Hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na dunia. Dunia ilikuwa bila umbo na tupu. Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji na roho ya Mungu ilikuwa ikitanda juu ya maji. Mungu akasema, “Mwanga uwe.” Mwanga ukawa. Mungu akauona mwanga kuwa ni mwema. Kisha Mungu akautenganisha mwanga na giza, mwanga akauita “Mchana” na giza akaliita “Usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya kwanza. Mungu akasema, “Anga liwe katikati ya maji, liyatenge maji sehemu mbili.” Mungu akalifanya anga, akayatenga maji yaliyo juu ya anga na yale yaliyo chini ya anga hilo. Ikawa hivyo. Mungu akaliita anga “Mbingu.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya pili. Mungu akasema, “Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, nchi kavu itokee.” Ikawa hivyo. Mungu akapaita mahali pakavu “Nchi” na kusanyiko la maji akaliita “Bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu akasema, “Nchi na ioteshe mimea. Mimea izaayo mbegu, na miti izaayo matunda yenye mbegu.” Ikawa hivyo. Basi, nchi ikaotesha mimea izaayo mbegu kwa jinsi yake, na miti izaayo matunda yenye mbegu kwa jinsi yake. Mungu akaona kuwa ni vyema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tatu. Mungu akasema, “Mianga na iweko angani, itenge mchana na usiku, ioneshe nyakati, majira, siku na miaka, na ingae angani na kuiangazia dunia.” Ikawa hivyo. Basi, Mungu akafanya mianga miwili mikubwa; ule mkubwa utawale mchana na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka mianga hiyo angani iiangazie dunia, ipate kutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akaona kuwa ni vyema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya nne. Mungu akasema, “Maji na yatoe makundi ya viumbe hai na ndege waruke angani.” Basi, Mungu akaumba wanyama wakubwa sana wa baharini na aina zote za viumbe vyote hai viendavyo na kujaa majini; akaumba na aina zote za ndege wote. Mungu akaona kuwa ni vyema. Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni, muongezeke, muyajaze maji ya bahari; nao ndege waongezeke katika nchi.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tano. Mungu akasema, “Nchi na itoe aina zote za viumbe hai, wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo na wanyama wa porini wa kila aina.” Ikawa hivyo. Basi, Mungu akafanya aina zote za wanyama wa porini, wanyama wa kufugwa, na viumbe vitambaavyo. Mungu akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu akasema, “Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa, dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo.” Basi, Mungu akaumba mtu kwa mfano wake; naam, kwa mfano wake Mungu alimuumba. Aliwaumba mwanamume na mwanamke. Mungu akawabariki na kuwaambia, “Zaeni muongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki; muwatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kitembeacho duniani.” Kisha Mungu akasema, “Tazama, nawapeni kila mmea duniani uzaao mbegu, na kila mti uzaao matunda yenye mbegu; mbegu zao au matunda yao yatakuwa chakula chenu. Nao wanyama wote duniani, ndege wote wa angani, viumbe vyote vitambaavyo, naam, kila kiumbe chenye uhai, chakula chao kitakuwa majani yote ya mimea.” Ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya kuwa ni chema kabisa. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya sita. Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyokamilika pamoja na vitu vyote vilivyomo. Siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyofanya; siku hiyo ya saba Mungu akapumzika baada ya kazi yake yote aliyofanya. Mungu akaibariki siku ya saba na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote ya kuumba. Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyoumbwa. Siku ile Mwenyezi-Mungu alipoziumba mbingu na dunia, Hapakuwa na mimea juu ya nchi wala miti haikuwa imechipua kwani Mwenyezi-Mungu hakuwa ameinyeshea nchi mvua, wala hapakuwa na mtu wa kuilima. Hata hivyo, maji yalitoka ardhini yakainywesha ardhi yote. Basi, Mwenyezi-Mungu akamfanya mwanamume kwa mavumbi ya udongo, akampulizia puani pumzi ya uhai, na huyo mwanamume akawa kiumbe hai. Kisha Mwenyezi-Mungu akapanda bustani huko Edeni, upande wa mashariki, na humo akamweka huyo mwanamume aliyemuumba. Mwenyezi-Mungu akaotesha kutoka ardhini kila aina ya miti mizuri izaayo matunda yafaayo kwa chakula. Katikati ya bustani hiyo kulikuwa na mti wa uhai na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Kulikuwa na mto huko Edeni uliotiririka maji na kuinywesha hiyo bustani; kutoka huko mto huo uligawanyika kuwa mito minne. Jina la mto wa kwanza ni Pishoni; huo waizunguka nchi yote ya Hawila ambako kuna dhahabu. Dhahabu ya nchi hiyo ni safi kabisa. Huko pia kuna marashi yaitwayo bedola na vito viitwavyo shohamu. Jina la mto wa pili ni Gihoni; huo waizunguka nchi yote ya Kushi. Jina la mto wa tatu ni Tigri, nao watiririkia upande wa mashariki wa nchi ya Ashuru; na jina la mto wa nne ni Eufrate. Basi, Mwenyezi-Mungu akamtwaa huyo mwanamume, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. Mwenyezi-Mungu alimwamuru huyo mwanamume, “Waweza kula matunda ya mti wowote katika bustani; lakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, usile, maana siku utakapokula matunda ya mti huo, hakika utakufa.” Kisha Mwenyezi-Mungu akasema, “Si vizuri huyu mwanamume kuwa peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.” Basi, kutoka katika udongo, Mwenyezi-Mungu akaumba kila mnyama wa porini na kila ndege wa angani, halafu akamletea huyo mwanamume aone atawapa majina gani; na majina aliyowapa viumbe hao, yakawa ndio majina yao. Basi, huyo mwanamume akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, wanyama wa porini na ndege wote wa angani. Lakini hakupatikana msaidizi yeyote wa kumfaa. Basi, Mwenyezi-Mungu akamletea huyo mwanamume usingizi mzito, na alipokuwa usingizini, akatwaa ubavu wake mmoja na kupafunika mahali pale kwa nyama. Na huo ubavu Mwenyezi-Mungu alioutoa kwa yule mwanamume akaufanya kuwa mwanamke, akamleta kwa huyo mwanamume. Ndipo huyo mwanamume akasema, “Naam! Huyu ni mfupa kutoka mifupa yangu, na nyama kutoka nyama yangu. Huyu ataitwa ‘Mwanamke ’, kwa sababu ametolewa katika mwanamume.” Ndiyo maana mwanamume humwacha baba yake na mama yake, akaambatana na mkewe, nao wawili huwa mwili mmoja. Huyo mwanamume na mkewe wote walikuwa uchi, lakini hawakuona haya. Nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini walioumbwa na Mwenyezi-Mungu. Basi, nyoka akamwambia huyo mwanamke, “Ati Mungu alisema msile matunda ya mti wowote bustanini?” Mwanamke akamjibu huyo nyoka, “Twaweza kula matunda ya mti wowote bustanini; lakini Mungu alisema, ‘Msile matunda ya mti ulio katikati ya bustani, wala msiuguse, msije mkafa.’” Nyoka akamwambia mwanamke, “Hamtakufa! Mungu alisema hivyo kwa sababu anajua kwamba mkila matunda ya mti huo mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumewe, naye pia akala. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakatambua kwamba wako uchi; hivyo wakajishonea majani ya mtini, wakajifanyia mavazi ya kiunoni. Jioni, wakati wa kupunga upepo, huyo mwanamume na mkewe wakasikia hatua za Mwenyezi-Mungu akitembea bustanini, nao wakajificha kati ya miti ya bustani, Mwenyezi-Mungu asipate kuwaona. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwita huyo mwanamume, “Uko wapi?” Naye akamjibu, “Nimesikia hatua zako bustanini, nikaogopa na kujificha, maana nilikuwa uchi.” Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umekula tunda la mti nililokuamuru usile?” Huyo mwanamume akajibu, “Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza huyo mwanamke, “Umefanya nini wewe?” Mwanamke akamjibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.” Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hivyo, umelaaniwa kuliko wanyama wote wa kufugwa, na kuliko wanyama wote wa porini. Kwa tumbo lako utatambaa, na kula vumbi siku zote za maisha yako. Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, kati ya uzawa wako na uzawa wake; yeye atakiponda kichwa chako, nawe utamwuma kisigino chake.” Kisha akamwambia mwanamke, “Nitakuzidishia uchungu wa kuzaa, kwa uchungu utazaa watoto. Hata hivyo utakuwa na hamu na mumeo, naye atakutawala.” Kisha akamwambia huyo mwanamume, “Kwa kuwa wewe umemsikiliza mkeo, ukala matunda ya mti ambayo nilikuamuru usile; kwa hiyo, kwa kosa lako ardhi imelaaniwa. Kwa jasho utajipatia humo riziki yako, siku zote za maisha yako. Ardhi itakuzalia michongoma na magugu, nawe itakubidi kula majani ya shambani. Kwa jasho lako utajipatia chakula mpaka utakaporudi udongoni ulimotwaliwa; maana wewe ni mavumbi, na mavumbini utarudi.” Adamu akampa mkewe jina “Hawa ”, kwani alikuwa mama wa binadamu wote. Mwenyezi-Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. Kisha Mwenyezi-Mungu akasema, “Sasa, binadamu amekuwa kama mmoja wetu, anajua mema na mabaya. Lazima kumzuia kula lile tunda la mti wa uhai, kwani akilila ataishi milele!” Basi, Mwenyezi-Mungu akamfukuza Adamu nje ya bustani ya Edeni, ili akailime ardhi ambamo alitwaliwa. Alimfukuza nje, na kuweka mlinzi upande wa mashariki wa bustani ya Edeni na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia iendayo kwenye mti wa uhai. Adamu akalala na Hawa mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Nimepata mtoto wa kiume kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu!” Halafu akamzaa Abeli nduguye. Abeli alikuwa mfugaji kondoo na Kaini alikuwa mkulima. Baada ya muda fulani, Kaini alimtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kutokana na mazao ya shambani, naye Abeli akamtolea Mungu sadaka ya wazawa wa kwanza wa kondoo wake na nyama nono. Mwenyezi-Mungu akapendezwa na Abeli na tambiko yake, lakini hakupendezwa na Kaini wala na tambiko yake. Basi, Kaini akakasirika sana na uso wake ukakunjamana. Mwenyezi-Mungu akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika, na kwa nini uso wako umekunjamana? Je, ukitenda vyema hutakubaliwa? Na usipotenda vyema, basi, dhambi inakuvizia mlangoni; inakutamani, lakini unapaswa kuishinda.” Baadaye, Kaini akamwambia Abeli nduguye, “Twende nje shambani ” Basi, walipokuwa shambani, Kaini akamvamia Abeli nduguye, akamuua. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Kaini akamjibu, “Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Mwenyezi-Mungu akasema, “Umefanya nini? Damu ya ndugu yako yanililia kutoka udongoni. Sasa wewe umelaaniwa! Hutailima tena ardhi yenye rutuba ambayo kama kinywa imeipokea damu ya nduguyo uliyemuua. Ukiilima ardhi haitakupatia tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani.” Kaini akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Adhabu yangu ni kubwa mno; siwezi kuistahimili. Leo umenifukuza kutoka ardhi yenye rutuba na mbali nawe. Basi, nitakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani, na yeyote atakayeniona ataniua.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sivyo! Atakayekuua wewe Kaini atalipizwa mara saba.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamtia Kaini alama ya tahadhari, ili yeyote atakayemwona asimuue. Kisha Kaini akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawa anaishi katika nchi ya Nodi, upande wa mashariki wa Edeni. Kaini akalala na mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Henoki. Kaini akajenga mji akauita kwa jina la Henoki mwanawe. Henoki akamzaa Iradi, naye Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, naye Methushaeli akamzaa Lameki. Lameki alioa wanawake wawili, mmoja aliitwa Ada na mwingine Sila. Ada alimzaa Yabali ambaye alikuwa baba yao wafugaji waishio mahemani. Ndugu yake alikuwa Yubali; huyo alikuwa baba yao wanamuziki wote wapigao zeze na filimbi. Sila naye alimzaa Tubal-kaini, ambaye alikuwa mhunzi wa vyombo vyote vya shaba na chuma. Dada yake Tubal-kaini alikuwa Naama. Lameki akawaambia wake zake, “Ada na Sila sikieni sauti yangu! Sikilizeni nisemayo enyi wake za Lameki. Mimi niliua mtu kwa kunijeruhi, naam, nilimuua kijana kwa kuniumiza. Ikiwa Kaini atalipizwa mara saba, kweli Lameki atalipizwa mara sabini na saba.” Adamu akalala tena na Hawa mkewe, naye akazaa mtoto wa kiume, akamwita Sethi akisema, “Mungu amenijalia mtoto mahali pa Abeli aliyeuawa na Kaini.” Sethi naye alipata mtoto wa kiume, akamwita Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kumwomba Mwenyezi-Mungu kwa jina lake. Ifuatayo ni orodha ya wazawa wa Adamu. Wakati Mungu alipomuumba binadamu, alimuumba kwa mfano wake. Aliwaumba mwanamume na mwanamke, kisha akawabariki na kuwapa jina “Binadamu.” Adamu alipokuwa na umri wa miaka 130, alipata mtoto aliyefanana naye, na mwenye sura kama yake; akamwita Sethi. Baada ya kumzaa Sethi, Adamu aliishi miaka 800, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Adamu alifariki akiwa na umri wa miaka 930. Sethi alipokuwa na umri wa miaka 105, alimzaa Enoshi. Baada ya kumzaa Enoshi, Sethi aliishi miaka 807, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Sethi alifariki akiwa na umri wa miaka 912. Enoshi alipokuwa na umri wa miaka 90, alimzaa Kenani. Baada ya kumzaa Kenani, Enoshi aliishi miaka 815 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Enoshi alifariki akiwa na umri wa miaka 905. Kenani alipokuwa na umri wa miaka 70, alimzaa Mahalaleli. Baada ya kumzaa Mahalaleli, Kenani aliishi miaka 840 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Kenani alifariki akiwa na umri wa miaka 910. Mahalaleli alipokuwa na umri wa miaka 65, alimzaa Yaredi. Baada ya kumzaa Yaredi, Mahalaleli aliishi miaka 830 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Mahalaleli alifariki akiwa na umri wa miaka 895. Yaredi alipokuwa na umri wa miaka 162, alimzaa Henoki. Baada ya kumzaa Henoki, Yaredi aliishi miaka 800 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Yaredi alifariki akiwa na umri wa miaka 962. Henoki alipokuwa na umri wa miaka 65, alimzaa Methusela. Henoki alikuwa mcha Mungu. Baada ya kumzaa Methusela, Henoki aliishi miaka 300 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Henoki aliishi miaka 365. Alikuwa mcha Mungu, akatoweka, kwa maana Mungu alimchukua. Wakati Methusela alipokuwa na umri wa miaka 187, alimzaa Lameki. Baada ya kumzaa Lameki, Methusela aliishi miaka 782, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Methusela alifariki akiwa na umri wa miaka 969. Wakati Lameki alipokuwa na umri wa miaka 182, alimzaa mtoto wa kiume. Alimwita mtoto huyo Noa, akisema, “Mtoto huyu ndiye atakayetufariji kutokana na kazi yetu ngumu tunayofanya kwa mikono yetu katika ardhi aliyoilaani Mwenyezi-Mungu.” Baada ya kumzaa Noa, Lameki aliishi miaka 595 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Lameki alifariki akiwa na umri wa miaka 777. Noa alipokuwa na umri wa miaka 500, alimzaa Shemu na Hamu na Yafethi. Binadamu walipozidi kuongezeka duniani na kuzaa wasichana, watoto wa kiume wa Mungu waliwaona hao wasichana wa watu kuwa ni wazuri, wakawachukua wale waliowapenda kuwa wake zao. Hapo Mwenyezi-Mungu akasema, “Roho yangu haitakaa ndani ya binadamu milele, maana yeye ni wa kufa tu. Basi, hataishi zaidi ya miaka 120.” Nyakati hizo na hata baadaye, kulikuwa na majitu duniani ambao walikuwa wazawa wa watoto wa kiume wa Mungu na wasichana wa watu. Hao ndio watu waliokuwa mashujaa na wenye sifa enzi hizo, nao waliitwa Wanefili. Mwenyezi-Mungu alipoona wingi wa uovu wa binadamu duniani, na kwamba kila analokusudia binadamu moyoni mwake ni ovu daima, Mwenyezi-Mungu alisikitika sana kwa kumuumba binadamu duniani. Mwenyezi-Mungu alihuzunika sana moyoni mwake, hivyo akasema, “Nitamfuta kabisa duniani binadamu niliyemuumba; nitafutilia mbali pia wanyama wa porini, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Ninasikitika kwamba niliwaumba duniani.” Lakini Noa alipata fadhili mbele ya Mwenyezi-Mungu. Ifuatayo ni habari juu ya Noa ambaye alikuwa ndiye mwadilifu pekee na ambaye hakuwa na lawama nyakati zake. Alikuwa mcha Mungu. Noa alikuwa na watoto watatu wa kiume: Shemu, Hamu na Yafethi. Mungu aliiona dunia kuwa imeharibika na kujaa ukatili. Naam, Mungu aliiangalia dunia, akaona kuwa imeharibika kabisa, kwa maana kila mtu alifuata njia yake mbovu. Mungu akamwambia Noa, “Nimeamua kuwaangamiza binadamu wote kwa sababu wameijaza dunia ukatili. Naam, nitawaangamiza kabisa pamoja na dunia! Kwa hiyo, jitengenezee safina kwa mbao za mpingo. Gawa vyumba ndani yake na ipake lami ndani na nje. Utaitengeneza hivi: Urefu wake mita 139, upana wake mita 25 na kimo chake mita 15. Safina hiyo iwe ya ghorofa tatu na yenye mlango pembeni. Itengenezee paa, kisha acha nafasi ipatayo nusu mita kati ya paa na dari. Nitaleta gharika ili kuangamiza viumbe vyote hai duniani. Kila kiumbe hai duniani kitakufa. Lakini nitafanya agano nawe. Utaingia katika safina, wewe pamoja na mkeo, wanao na wake zao. Nawe utaingiza katika safina jozi ya kila aina ya viumbe, wa kiume na wa kike, ili kuwahifadhi hai pamoja nawe. “Utaingiza kila aina ya ndege wa angani, kila aina ya mnyama, kila aina ya kiumbe kitambaacho, wawiliwawili, ili kuwahifadhi hai. Pia chukua aina zote za vyakula vinavyolika, uvihifadhi kwa ajili ya chakula chenu na viumbe hao.” Noa akafanya yote kama Mungu alivyomwamuru. Mwenyezi-Mungu akamwambia Noa, “Ingia ndani ya safina wewe pamoja na jamaa yako yote, kwa maana, kati ya watu wote wanaoishi nyakati hizi zako, nimekuona wewe peke yako kuwa mwadilifu mbele yangu. Chukua pamoja nawe wanyama wote walio safi, dume na jike, saba saba; lakini wanyama walio najisi, chukua dume na jike, wawiliwawili. Vilevile chukua ndege wa angani dume na jike, saba saba, ili kuzihifadhi hai aina zao duniani. Baada ya siku saba, nitanyesha mvua nchini siku arubaini mchana na usiku, na kila kiumbe hai nilichokiumba duniani nitakiangamiza.” Noa akafanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru. Noa alikuwa na umri wa miaka 600 wakati gharika ilipotokea nchini. Noa, mkewe, wanawe na wake zao wakaingia ndani ya safina ili kuiepa gharika. Wanyama walio safi, wanyama walio najisi, ndege na viumbe vyote vitambaavyo, wawiliwawili, dume na jike, wakaingia ndani ya safina pamoja na Noa kama Mungu alivyomwamuru. Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaanza kuifunika nchi. Noa alipokuwa na umri wa miaka 600, mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili, siku hiyo chemchemi zote za vilindi vya nchi zikabubujika maji, na madirisha ya mbinguni yakafunguka. Mvua ikanyesha nchini siku arubaini mchana na usiku. Siku hiyohiyo mvua ilipoanza kunyesha, Noa, mkewe na wanawe, Shemu, Hamu na Yafethi, pamoja na wake zao, waliingia ndani ya safina. Waliingia wao wenyewe pamoja na aina zote za wanyama wa porini, wanyama wafugwao, wanyama watambaao na ndege wa kila aina. Waliingia ndani ya safina pamoja na Noa wiliwawili wa kila aina ya viumbe hai. Kila aina yao waliingia, dume na jike, kama Mungu alivyomwamuru Noa. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaufunga mlango wa safina nyuma yake Noa. Gharika ilidumu nchini kwa muda wa siku arubaini. Maji yakaongezeka na kuiinua safina, ikaelea juu ya ardhi. Maji yakaendelea kuongezeka zaidi nchini na safina ikaelea juu yake. Maji hayo yakawa mengi sana juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu katika nchi. Yaliongezeka hata kuifunika milima kiasi cha mita saba na nusu. Viumbe wote hai katika nchi wakafa. Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama wa porini, makundi ya viumbe wote katika nchi kavu na wanadamu wote; naam, kila kiumbe hai katika nchi kavu kilikufa. Mungu akaangamiza kila kiumbe kilichokuwa hai duniani: Binadamu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Vyote viliangamizwa duniani. Noa tu ndiye aliyesalimika na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Maji hayo yalidumu katika nchi siku 150. Kisha Mungu akamkumbuka Noa na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Basi, Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakaanza kupungua. Chemchemi za maji ya vilindi na madirisha ya mbinguni yakafungwa. Mvua ikazuiwa, maji yakaendelea kupungua polepole katika nchi. Baada ya siku 150, maji yakawa yamepungua sana. Mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua juu ya milima ya Ararati. Maji yakaendelea kupungua polepole, na siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana. Baada ya siku arubaini, Noa alifungua dirisha alilokuwa ametengeneza katika hiyo safina, akamtoa kunguru nje, naye hakurudi bali aliruka huko na huko mpaka maji yalipokauka nchini. Kisha Noa akamtoa njiwa apate kuona kama maji yalikuwa yamepungua juu ya nchi. Lakini, kwa vile maji yalikuwa bado yameifunika nchi yote, huyo njiwa hakupata mahali pa kutua, akamrudia Noa katika safina. Noa akanyosha mkono, akamtwaa na kumrudisha ndani ya safina. Noa akangoja siku nyingine saba, kisha akamtoa tena huyo njiwa. Njiwa huyo akamrudia Noa saa za jioni akiwa na tawi bichi la mzeituni mdomoni mwake. Kwa hiyo Noa akajua kwamba maji yalikuwa yamepungua katika nchi. Kisha akangoja siku nyingine saba, akamtoa tena yule njiwa; safari hii njiwa hakurudi kabisa. Noa alipokuwa na umri wa miaka 601, siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, maji yalikuwa yamekauka katika nchi. Noa akafunua kifuniko cha safina na alipotazama, akaona kwamba nchi ilikuwa imekauka. Siku ya 27 ya mwezi wa pili, nchi ilikuwa imekauka kabisa. Hapo, Mungu akamwambia Noa, “Toka katika safina, wewe pamoja na mkeo, wanao na wake zao. Toa pia viumbe wote hai wa kila aina waliokuwa pamoja nawe, ndege na wanyama na kila kiumbe kitambaacho, wapate kuzaa kwa wingi duniani, waongezeke na kuenea kila mahali duniani.” Basi, Noa akatoka katika safina pamoja na wanawe na mkewe pamoja na wake za wanawe. Wakatoka kufuatana na jamii zao, wanyama wote wa porini, viumbe wote watambaao, ndege wote na wanyama wote hai duniani. Noa akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu, akatwaa mmoja katika kila aina ya wanyama walio safi na ndege walio safi, akamtolea Mungu sadaka za kuteketezwa. Harufu nzuri ya tambiko hiyo ikampendeza Mwenyezi-Mungu, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena nchi kwa sababu ya binadamu; najua kwamba mawazo yake ni maovu tangu utoto wake. Wala sitaangamiza tena viumbe wote kama nilivyofanya. Kadiri itakavyodumu nchi majira ya kupanda na kuvuna, ya baridi na joto, ya masika na kiangazi, usiku na mchana, hayatakoma.” Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni, muongezeke, mkaijaze nchi. Wanyama wote, ndege wote wa angani, viumbe wote watambaao juu ya nchi na samaki wote wa baharini watakuwa na hofu na kuwaogopa nyinyi. Wote wamewekwa chini ya mamlaka yenu. Wanyama wote hai watakuwa chakula chenu kama vile nilivyowapa mimea kuwa chakula chenu. Lakini msile nyama yenye damu, kwani uhai uko katika damu. Damu ya uhai wenu nitaidai; nitaidai kutoka kwa kila mnyama na binadamu. Atakayemuua binadamu mwenzake, nitamdai uhai wake. Amwagaye damu ya binadamu, damu yake itamwagwa na binadamu; maana binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu. Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni kwa wingi, mkaongezeke nchini.” Kisha Mungu akamwambia Noa na wanawe, “Ninaweka agano langu nanyi na wazawa wenu na viumbe vyote hai: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wa porini, wote waliotoka katika safina pamoja nanyi. Nathibitisha agano langu nanyi, kwamba, kamwe viumbe vyote hai havitaangamizwa kwa gharika, wala haitatokea tena gharika kuiharibu nchi.” Tena Mungu akasema, “Hii ndiyo alama ya agano ninalofanya kati yangu nanyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi kwa vizazi vyote vijavyo. Naweka upinde wangu mawinguni, nao utakuwa ishara ya agano kati yangu na dunia. Kila nitakapoifunika dunia kwa mawingu, na huo upinde wa mvua utakapoonekana katika mawingu, nitalikumbuka agano langu nanyi na viumbe vyote hai. Kamwe maji hayatageuka kuwa gharika ya kuviangamiza viumbe vyote hai. Huo upinde utakapotokea mawinguni, nitauona na kulikumbuka agano hilo la milele kati yangu na viumbe vyote hai duniani.” Mungu akamwambia Noa, “Hii ndiyo ishara ya agano ambalo nimefanya na viumbe vyote hai duniani.” Watoto wa Noa waliotoka katika safina walikuwa Shemu, Hamu na Yafethi. Hamu alikuwa baba yake Kanaani. Hao ndio watoto watatu wa Noa, na kutokana nao watu walienea duniani kote. Noa alikuwa mkulima wa kwanza. Alilima shamba la mizabibu, akanywa divai, akalewa, kisha akalala uchi hemani mwake. Hamu, baba yake Kanaani, aliuona uchi wa baba yake, akatoka nje na kuwaambia ndugu zake wawili. Lakini Shemu na Yafethi wakatwaa nguo, wakaitanda mabegani mwao, wakaenda kinyumenyume na kuufunika uchi wa baba yao. Waliangalia pembeni, wala hawakuuona uchi wa baba yao. Noa alipolevuka na kujua alivyotendewa na mwanawe mdogo, akasema, “Kanaani na alaaniwe! Atakuwa mtumwa wa watumwa kwa ndugu zake.” Tena akasema, “Shemu na abarikiwe na Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu! Kanaani na awe mtumwa wake. Mungu na amkuze Yafethi, aishi katika hema za Shemu; Kanaani na awe mtumwa wake.” Baada ya gharika, Noa aliishi miaka 350, kisha akafariki akiwa na umri wa miaka 950. Baada ya gharika, watoto wa Noa, Shemu, Hamu na Yafethi, walipata watoto wa kiume na wa kike. Hii ndiyo orodha ya wazawa wao: Watoto wa kiume wa Yafethi walikuwa Gomeri, Magogu, Madai, Yavani, Tubali, Mesheki na Tirasi. Watoto wa kiume wa Gomeri walikuwa Ashkenazi, Rifathi na Togama. Watoto wa kiume wa Yavani walikuwa Elisha, Tarshishi, Kitimu na Dodanimu. Hawa ndio asili ya watu walioenea sehemu za pwani, kila watu kwa lugha yao, kwa jamaa zao na kufuata mataifa yao. Watoto wa kiume wa Hamu walikuwa Kushi, Misri, Puti na Kanaani. Watoto wa kiume wa Kushi walikuwa Seba, Hawila, Sabta, Raama na Sabteka. Watoto wa kiume wa Raama walikuwa Sheba na Dedani. Kushi alikuwa baba yake Nimrodi ambaye alikuwa shujaa wa kwanza duniani. Alikuwa mwindaji shujaa mbele ya Mwenyezi-Mungu, ndiyo maana kuna msemo usemao, “Kama Nimrodi mwindaji shujaa mbele ya Mwenyezi-Mungu.” Miji ya kwanza ya utawala wake ilikuwa Babuloni, Ereki na Akadi, katika nchi ya Shinari. Kutoka huko, Nimrodi alikwenda Ashuru, akajenga miji ya Ninewi, Rehoboth-iri, Kala na Reseni ulioko kati ya Ninewi na mji mkubwa wa Kala. Misri alikuwa babu wa Waludi, Waanamu, Walehabi, Wanaftuhi, Wapathrusi, Wakasluhi (ambao ndio asili ya Wafilisti), na Wakaftori. Kanaani alikuwa babu yake Sidoni, mzaliwa wake wa kwanza, na Hethi, na pia babu yao Wayebusi, Waamori, Wagirgashi, Wahivi, Waarki, Wasini, Waarvadi, Wasemari na Wahamathi. Baadaye watu wa jamii mbalimbali za Kanaani walitawanyika, hata eneo la nchi yao likawa toka Sidoni kuelekea kusini, hadi Gerari mpaka Gaza, na kuelekea mashariki hadi Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu hadi Lasha. Hao ndio wazawa wa Hamu kadiri ya makabila yao, lugha zao, nchi zao na mataifa yao. Shemu, mkubwa wa Yafethi, alikuwa baba yao Waebrania wote. Watoto wa kiume wa Shemu walikuwa Elamu, Ashuru, Arfaksadi, Ludi na Aramu. Watoto wa kiume wa Aramu walikuwa Usi, Huli, Getheri na Mashi. Arfaksadi alimzaa Shela, Shela akamzaa Eberi. Eberi alikuwa na watoto wa kiume wawili; wa kwanza akamwita Pelegi kwa sababu wakati huo watu duniani waligawanyika, na wa pili akamwita Yoktani. Yoktani alikuwa baba wa Almodadi, Shelefu, Hasarmawethi, Yera, Hadoramu, Uzali, Dikla, Obali, Abimaeli, Sheba, Ofiri, Hawila na Yobabu. Hao wote walikuwa watoto wa Yoktani. Nchi walimokaa ilienea toka Mesha mpaka Sefari katika nyanda za juu za mashariki. Hao ndio wazawa wa Shemu, kadiri ya makabila yao, lugha zao, nchi zao na mataifa yao. Hao ndio jamaa za watoto wa Noa, kadiri ya vizazi vyao na mataifa yao. Kutokana nao mataifa yote yalienea duniani baada ya gharika. Kwanza, watu wote duniani walikuwa na lugha moja na walitumia maneno yaleyale. Basi, ikawa watu waliposafirisafiri kutoka mashariki, walifika katika nchi tambarare huko Shinari, wakakaa. Kisha wakaambiana, “Haya! Na tufyatue matofali, tuyachome moto vizuri.” Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. Wakasema, “Na tujijengee mji na mnara ambao kilele chake kitafika mbinguni ili tujipatie jina, tusije tukatawanyika duniani kote.” Ndipo Mwenyezi-Mungu akashuka chini kuuona mji huo na mnara walioujenga binadamu. Mwenyezi-Mungu akasema, “Tazama, watu hawa ni taifa moja na wote wana lugha moja; huu ni mwanzo tu wa yale watakayoyafanya. Lolote wanalokusudia kulifanya watafanikiwa. Haya, na tushuke chini na kuivuruga lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.” Hivyo, Mwenyezi-Mungu akawatawanya mahali pote duniani, nao wakaacha kuujenga ule mji. Mji huo ukaitwa Babeli, kwa sababu huko ndiko Mwenyezi-Mungu alikoivuruga lugha ya dunia yote, na kutoka huko akawatawanya watu kila mahali duniani. Wafuatao ni wazawa wa Shemu. Miaka miwili baada ya ile gharika, Shemu akiwa na umri wa miaka 100, alimzaa Arfaksadi. Baada ya kumzaa Arfaksadi, Shemu aliishi miaka 500 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Arfaksadi alipokuwa na umri wa miaka 35, alimzaa Shela. Baada ya kumzaa Shela, Arfaksadi aliishi miaka 403 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Shela alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Eberi. Baada ya kumzaa Eberi, Shela aliishi miaka 403 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Eberi alipokuwa na umri wa miaka 34, alimzaa Pelegi. Baada ya kumzaa Pelegi, Eberi aliishi miaka 430 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Pelegi alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Reu. Baada ya kumzaa Reu, Pelegi aliishi miaka 209 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Reu alipokuwa na umri wa miaka 32, alimzaa Serugi. Baada ya kumzaa Serugi, Reu aliishi miaka 207 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Serugi alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Nahori. Baada ya kumzaa Nahori, Serugi aliishi miaka 200 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Nahori alipokuwa na umri wa miaka 29, alimzaa Tera. Baada ya kumzaa Tera, Nahori aliishi miaka 119, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike. Tera alipokuwa na umri wa miaka 70, alimzaa Abramu na Nahori na Harani. Wafuatao ni wazawa wa Tera, baba yao Abramu, Nahori na Harani. Harani alikuwa baba yake Loti. Huyo Harani alifariki wakati Tera baba yake alikuwa anaishi huko Uri alikokuwa amezaliwa. Abramu na Nahori walioa. Mke wa Abramu aliitwa Sarai. Mke wa Nahori aliitwa Milka, binti Harani ambaye pia alikuwa baba yake Iska. Sarai hakuwa na mtoto kwa sababu alikuwa tasa. Tera akamchukua Abramu mwanawe, Loti mjukuu wake aliyekuwa mwanawe Harani, na Sarai mkewe Abramu, wakaondoka wote pamoja toka Uri, mji wa Wakaldayo, wakaenda katika nchi ya Kanaani. Lakini walipofika Harani, wakakaa. Tera alifariki huko Harani akiwa na umri wa miaka 205. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, acha jamaa yako na nyumba ya baba yako, uende katika nchi nitakayokuonesha. Nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, nitakubariki na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka. Anayekubariki, nitambariki; anayekulaani, nitamlaani. Kwako wewe, nitayabariki mataifa yote ya dunia.” Kwa hiyo, Abramu akaondoka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru; na Loti akaenda pamoja naye. Abramu alikuwa na umri wa miaka 75 alipotoka Harani. Alimchukua Sarai mkewe, na Loti mwana wa ndugu yake, pamoja na mali yao yote na watu wote waliokuwa wamejipatia huko Harani, wakaondoka kuelekea nchi ya Kanaani. Walipoingia nchini Kanaani, Abramu akapita katikati ya nchi mpaka Shekemu, mahali patakatifu, penye mti wa mwaloni wa More. Wakati huo, Wakanaani walikuwa ndio wenyeji wa nchi hiyo. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamtokea Abramu, akamwambia, “Wazawa wako nitawapa nchi hii.” Basi, Abramu akajenga madhabahu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu aliyemtokea. Baadaye Abramu akaondoka, akaelekea mlimani mashariki ya Betheli akapiga hema kati ya mji wa Betheli, upande wa magharibi, na mji wa Ai upande wa mashariki. Hapo pia akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu na kumwomba kwa jina lake. Kisha Abramu akaendelea kusafiri kuelekea upande wa Negebu. Wakati huo, njaa ilitokea nchini. Njaa hiyo ilikuwa kali, hivyo Abramu akalazimika kwenda Misri kukaa huko kwa muda. Alipokaribia Misri, Abramu alimwambia Sarai mkewe, “Najua kuwa wewe ni mwanamke mzuri na wa kuvutia. Wamisri watakapokuona watasema, ‘Huyu ni mkewe,’ kisha wataniua lakini wewe watakuacha hai. Basi, waambie kuwa wewe ni dada yangu ili mambo yaniendee vema, niachwe niishi kwa ajili yako.” Basi, Abramu alipowasili nchini Misri, wenyeji wa huko walimwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana. Maofisa wa Farao walipomwona Sarai, wakamsifia kwa Farao. Basi, Sarai akapelekwa nyumbani kwa Farao. Basi, kwa ajili yake, Farao alimfadhili Abramu, akampa kondoo, ng'ombe, punda dume, watumishi wa kiume na wa kike, punda jike na ngamia. Lakini Mwenyezi-Mungu akamtesa Farao na watu wote wa nyumba yake kwa mapigo makali kwa sababu ya Sarai, mkewe Abramu. Farao akamwita Abramu, akamwuliza, “Ni kitu gani hiki ulichonitendea? Mbona hukunijulisha kwamba Sarai ni mkeo? Kwa nini ulisema ni dada yako hata nikamchukua kuwa mke wangu? Basi, sasa mkeo ndiye huyo. Mchukue uende zako!” Kisha Farao aliwaamuru watu wake, nao wakamsindikiza Abramu njiani akiwa na mke wake na mali yake yote. Abramu akarudi kutoka Misri, akaingia upande wa Negebu. Alikuwa na mkewe na mali yake yote pamoja na Loti. Wakati huo, Abramu alikuwa ametajirika sana. Alikuwa na mifugo, fedha na dhahabu. Akaendelea kusafiri toka eneo la Negebu hadi Betheli. Alifika mahali alipokuwa amepiga kambi ya hema hapo awali, kati ya Betheli na Ai, ambapo alikuwa amejenga madhabahu. Hapo Abramu akamwomba Mwenyezi-Mungu kwa jina lake. Kadhalika, Loti, ambaye alifuatana na Abramu, alikuwa na kondoo, mifugo na hema. Idadi ya mifugo yao ilikuwa kubwa mno hata nchi ile haikuweza kuwatosha Abramu na Loti kuishi pamoja. Basi, kukazuka ugomvi kati ya wachungaji wa Abramu na wachungaji wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo. Basi, Abramu akamwambia Loti, “Kusiwe na mafarakano kati yetu wala kati ya wachungaji wako na wachungaji wangu, kwa sababu sisi ni jamaa moja. Tazama nchi hii yote mbele yako. Na tutengane. Ukienda kushoto, mimi nitakwenda kulia; ukienda kulia, mimi nitakwenda kushoto.” Loti akatazama, akaliona bonde la mto Yordani, akaona kuwa lina maji ya kutosha kila mahali, kama bustani ya Mwenyezi-Mungu na kama nchi ya Misri upande wa Soari. (Hii ilikuwa kabla Mwenyezi-Mungu hajaiangamiza miji ya Sodoma na Gomora). Kwa hiyo, Loti akajichagulia bonde lote la mto Yordani, akaelekea mashariki, na hivyo wakatengana. Abramu akabaki nchini Kanaani na Loti akakaa kati ya miji iliyokuwa bondeni, akahamishia kambi yake Sodoma. Watu wa Sodoma walikuwa waovu na watenda dhambi wakuu dhidi ya Mwenyezi-Mungu. Baada ya Loti kujitenga na Abramu, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Angalia toka hapo ulipo utazame pande zote: Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi. Nchi hii yote unayoiona nitakupa wewe na wazawa wako iwe yenu milele. Wazawa wako nitawafanya wawe wengi wasiohesabika, kama vile mavumbi ya nchi yasivyoweza kuhesabika! Basi, inuka uitembelee nchi hii katika mapana na marefu, kwani nitakupa wewe.” Kwa hiyo, Abramu akangoa hema, akaenda kukaa karibu na mialoni ya Mamre kule Hebroni; huko akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu. Wakati huo, mfalme Amrafeli wa Shinari, mfalme Arioko wa Elasari, mfalme Kedorlaomeri wa Elamu na mfalme Tidali wa Goiimu, walipigana vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, dhidi ya Birsha mfalme wa Gomora, Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboimu, na dhidi ya mfalme wa Bela (yaani Soari). Wafalme hao watano waliyaunganisha majeshi yao katika bonde la Sidimu (yaani Bahari ya Chumvi). Kwa muda wa miaka kumi na miwili walikuwa wakimtii mfalme Kedorlaomeri, lakini mnamo mwaka wa kumi na tatu, walimwasi. Mnamo mwaka wa kumi na nne, mfalme Kedorlaomeri na wale wafalme wenzake walikuja na kuwashinda watu wa Refaimu huko Ashtaroth-karnaimu, na Wazuzi huko Hamu, na Waemi huko Shawe-kiriathaimu, na Wahori huko mlimani kwao Seiri, wakawafukuza hadi Elparani, mpakani mwa jangwa. Kisha wakarudi nyuma mpaka Enmishpati (yaani Kadeshi), wakaivamia nchi yote ya Waamaleki, na kuwashinda Waamori waliokaa Hasason-tamari. Ndipo mfalme wa Sodoma, mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboimu na mfalme wa Bela (yaani Soari), wakaingia vitani katika bonde la Sidimu kupigana na Kedorlaomeri mfalme wa Elamu, Tidali mfalme wa Goiimu, Amrafeli mfalme wa Shinari na Arioko mfalme wa Elasari; wafalme wanne dhidi ya wafalme watano. Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami; kwa hiyo wafalme wa Sodoma na Gomora walipokuwa wakiikimbia vita, wakatumbukia humo, lakini wengine wakatorokea mlimani. Basi, wale walioshinda, wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora, kadhalika na mazao yao, wakaenda zao. Walimteka hata Loti, mwana wa nduguye Abramu aliyekuwa anakaa Sodoma, pamoja na mali yake, wakaenda zao. Mtu mmoja aliyeponyoka, akaenda kumwarifu yule Mwebrania Abramu ambaye alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mwamori Mamre. Mamre alikuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri. Wote walikuwa wamefanya agano na Abramu. Abramu alipopata habari kwamba mpwa wake amechukuliwa mateka, akatoka na watu wake stadi 318 waliozaliwa katika nyumba yake, akawafuatia adui mpaka Dani. Huko, akaligawa jeshi lake katika makundi. Usiku, akawashambulia adui zake, akawashinda na kuwafukuza hadi Hoba, kaskazini mwa Damasko. Basi, Abramu akaikomboa mali yote iliyotekwa na adui, na kumkomboa Loti mpwa wake, mali yake, pamoja na wanawake na watu wengine. Abramu aliporudi baada ya kumshinda mfalme Kedorlaomeri na wenzake, mfalme wa Sodoma alitoka kwenda kumlaki katika bonde la Shawe, (yaani Bonde la Mfalme). Naye Melkisedeki, mfalme wa mji wa Salemu, ambaye alikuwa kuhani wa Mungu Mkuu, akaleta mkate na divai, akambariki Abramu akisema, “Abramu na abarikiwe na Mungu Mkuu, Muumba mbingu na dunia! Na atukuzwe Mungu Mkuu, aliyewatia adui zako mikononi mwako!” Naye Abramu akampa Melkisedeki mchango wake sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu, lakini jichukulie mali yote wewe mwenyewe.” Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu, aliyeumba mbingu na dunia, kwamba sitachukua uzi au kamba ya kiatu, wala chochote kilicho chako, usije ukajivuna na kusema kwamba umenitajirisha. Basi, sitachukua chochote isipokuwa tu vile vitu vijana wangu walivyokula na sehemu ya wale waliokuwa pamoja nami, Aneri, Eshkoli na Mamre ambao wana haki nayo.” Baada ya mambo hayo, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Abramu katika maono, “Abramu! Usiogope! Mimi ni ngao yako. Tuzo lako litakuwa kubwa!” Lakini Abramu akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, utanipa nini hali naendelea kuishi bila mtoto, na mrithi wangu ni Eliezeri wa Damasko? Tazama! Hujanijalia mtoto; mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye atakayekuwa mrithi wangu!” Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Huyu hatakuwa mrithi wako! Mwanao halisi ndiye atakayekuwa mrithi wako.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamleta Abramu nje na kumwambia, “Tazama mbinguni! Zihesabu nyota, kama kweli utaweza kuzihesabu! Hivyo ndivyo wazawa wako watakavyokuwa wengi!” Abramu akamwamini Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akamkubali Abramu kuwa mwadilifu. Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu niliyekuleta toka Uri, mji wa Wakaldayo, ili nikupe nchi hii uimiliki.” Lakini Abramu akamwambia, “Ee Mwenyezi-Mungu, nitajuaje kwamba nitaimiliki nchi hii?” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Niletee ndama wa miaka mitatu, mwanambuzi jike wa miaka mitatu, kondoo dume wa miaka mitatu, na hua na kinda la njiwa.” Abramu akamletea hao wote, akamkata kila mnyama vipande viwili, akavipanga katika safu mbili, vikielekeana; lakini ndege hakuwakata vipande viwili. Na tai walipoijia hiyo mizoga, Abramu akawa anawafukuza. Jua lilipokuwa likitua, Abramu alishikwa na usingizi mzito; hofu na giza nene vikamfunika. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Ujue hakika ya kwamba wazawa wako watakaa kama wageni katika nchi isiyo yao, watakuwa watumwa na watateswa kwa muda wa miaka 400. Hata hivyo, nitaliadhibu taifa watakalolitumikia, na hatimaye watatoka wakiwa na mali nyingi. Lakini wewe mwenyewe utaishi maisha marefu na kufariki kwa amani. Wazawa wako watarudi hapa katika kizazi cha nne, kwa sababu uovu wa Waamori haujakamilika bado.” Jua lilipokwisha tua na giza kuingia, tanuri ifukayo moshi na mwenge uwakao moto vikapita katikati ya vile vipande vya nyama. Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu akafanya agano na Abramu akisema, “Wazawa wako ninawapa nchi hii, toka mto wa Misri hadi ule mto mkubwa wa Eufrate, yaani nchi za Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni, Wahiti, Waperizi, Warefai, Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.” Basi, Sarai, mkewe Abramu, alikuwa bado hajamzalia mumewe mtoto. Lakini alikuwa na mjakazi aliyeitwa Hagari, kutoka Misri. Basi, Sarai akamwambia Abramu, “Unajua kuwa Mwenyezi-Mungu hajanijalia kupata watoto. Mchukue Hagari mjakazi wangu; huenda nikapata watoto kwake.” Abramu akakubali shauri la Sarai. Kisha, Sarai akampa Abramu Hagari, mjakazi wake ambaye alikuwa Mmisri, awe mke wake. Haya yalitokea baada ya Abramu kukaa katika nchi ya Kanaani kwa muda wa miaka kumi. Abramu akamchukua Hagari, naye Hagari akapata mimba. Lakini mara tu alipoona amepata mimba, Hagari akaanza kumdharau bimkubwa wake. Sarai akamwambia Abramu, “Wewe utawajibika kwa ubaya ninaotendewa. Mimi nilikupa mjakazi wangu, lakini alipopata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake! Mwenyezi-Mungu na ahukumu kati yako na mimi!” Lakini Abramu akamwambia Sarai, “Mjakazi wako yuko chini ya mamlaka yako; mfanyie upendavyo.” Basi, Sarai akamtesa Hagari mpaka akatoroka. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamkuta Hagari penye chemchemi ya maji jangwani, chemchemi iliyoko njiani kuelekea Shuri. Malaika akamwuliza, “Hagari, mjakazi wa Sarai! Unatoka wapi na unakwenda wapi?” Hagari akamjibu, “Namkimbia bimkubwa wangu Sarai.” Yule malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa bimkubwa wako Sarai na umtii.” Zaidi ya hayo, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Hagari, “Nitawazidisha wazawa wako hata wasiweze kuhesabika kwa wingi wao.” Kisha huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Wewe ni mjamzito na utajifungua mtoto wa kiume; utamwita Ishmaeli, maana Mwenyezi-Mungu amesikia mateso yako. Ishmaeli ataishi kama pundamwitu; atakuwa adui wa kila mtu na kila mtu atakuwa adui yake. Ataishi akiwa adui wa jamaa yake.” Basi, Hagari akampa jina Mwenyezi-Mungu aliyezungumza naye huko, “Wewe ni Mungu Aonaye” kwa maana alifikiri, “Kweli hapa nimemwona yeye anionaye!” Ndiyo maana kile kisima chaitwa Beer-lahai-roi. Kisima hiki kipo kati ya Kadeshi na Beredi. Hagari akamzalia Abramu mtoto wa kiume. Abramu akamwita mtoto huyo Ishmaeli. Abramu alikuwa na umri wa miaka 86 wakati Hagari alipomzaa Ishmaeli. Wakati Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa, Mwenyezi-Mungu alimtokea, akamwambia, “Mimi ni Mungu mwenye nguvu. Fuata mwongozo wangu na kuishi bila lawama. Nami nitafanya agano nawe na kuwazidisha wazawa wako.” Hapo Abramu akasujudu. Naye Mungu akamwambia, “Ninafanya agano hili nawe: Utakuwa baba wa mataifa mengi. Tangu sasa, hutaitwa tena Abramu, bali utaitwa Abrahamu, maana nimekufanya kuwa baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na wazawa wengi sana; kwako nitazusha mataifa mengi na wafalme. Nitalithibitisha agano langu nawe, wazawa wako na vizazi vyao vyote milele; tena nitakuwa Mungu wako na Mungu wa wazawa wako milele. Nitakupa wewe na wazawa wako nchi hii ambamo unaishi kama mgeni; yaani nchi yote ya Kanaani iwe mali yenu milele; nami nitakuwa Mungu wao.” Kisha Mungu akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wako, wewe utalishika agano langu, wewe binafsi, wazawa wako na vizazi vyao vyote. Hili ndilo agano utakaloshika kati yangu na wewe na wazawa wako: Kila mwanamume miongoni mwenu lazima atahiriwe. Mtatahiriwa kwa kukata magovi yenu, na hii itakuwa ndiyo alama ya agano kati yangu nanyi. Kila mtoto wa kiume wa siku nane miongoni mwenu ni lazima atahiriwe. Kila mwanamume katika vizazi vyenu, awe mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwenu au aliyenunuliwa kwa fedha zenu kutoka kwa mgeni asiye mzawa wako; naam, kila mmoja wao aliyezaliwa katika nyumba yako na hata aliyenunuliwa kwa fedha zako ni lazima atahiriwe. Hiyo ni alama ya agano langu katika miili yenu, agano la milele. Mwanamume yeyote asiyetahiriwa atatengwa na watu, kwani atakuwa amevunja agano langu.” Kisha Mungu akamwambia Abrahamu, “Kuhusu mkeo, hutamwita tena jina lake Sarai, bali jina lake litakuwa Sara. Nitambariki, naye atakuzalia mtoto wa kiume. Naam, nitambariki Sara, naye atakuwa mama wa mataifa mengi na wafalme wa mataifa watatoka kwake.” Hapo Abrahamu akasujudu, akacheka moyoni mwake akiwaza, “Ati, itawezekana kweli mtoto kuzaliwa kwa mzee wa miaka 100? Na je, Sara ambaye umri wake ni miaka tisini, ataweza kupata mtoto?” Basi, Abrahamu akamwambia Mungu, “Laiti ungekubali ahadi yako hiyo imhusu Ishmaeli.” Mungu akamjibu, “La! Ila mkeo Sara atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita Isaka Nitaliimarisha agano langu kwake na wazawa wake, kuwa agano la milele. “Na, kuhusu Ishmaeli, nimesikia ombi lako. Nitambariki, nitamjalia watoto wengi na kuwazidisha sana. Ishmaeli atakuwa baba wa watawala kumi na wawili, nami nitamfanya kuwa baba wa taifa kubwa. Lakini agano langu litathibitika kwa Isaka ambaye Sara atakuzalia mwakani wakati kama huu.” Basi, Mungu alipomaliza kuongea, akamwacha Abrahamu. Kisha, siku hiyohiyo, Abrahamu akamtahiri mwanawe Ishmaeli na kuwatahiri watumwa wote wa kiume waliozaliwa nyumbani mwake na walionunuliwa kwa fedha zake, kama Mungu alivyomwamuru. Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 99 alipotahiriwa. Na Ishmaeli mwanawe alikuwa na umri wa miaka 13 alipotahiriwa. Abrahamu na mwanawe Ishmaeli pamoja na wanaume wote wa nyumba yake, watumwa wote waliozaliwa nyumbani mwake na walionunuliwa kwa fedha zake walitahiriwa siku hiyohiyo. Mwenyezi-Mungu alimtokea Abrahamu penye mialoni ya Mamre. Abrahamu alikuwa ameketi penye mlango wa hema lake wakati wa joto la mchana, na alipoinua macho yake, akaona watu watatu wamesimama mbali kidogo mbele yake. Mara alipowaona, akapiga mbio kutoka mlangoni mwa hema lake, akaenda kuwalaki. Alipowafikia aliinama kwa heshima na kusema, “Bwana zangu, kama mnanipenda tafadhali msinipite mimi mtumishi wenu ila mshinde kwangu. Mtaletewa maji kidogo ili mnawe miguu na kupumzika chini ya mti. Wakati mnapopumzika, nitaandaa chakula kidogo, mle, ili mpate nguvu za kuendelea na safari yenu; maana mmenijia mimi mtumishi wenu.” Nao wakasema, “Sawa! Fanya kama ulivyosema.” Abrahamu akarudi haraka hemani akamwambia Sara, “Tayarisha haraka vipimo vitatu vya unga bora, uukande, uoke mikate.” Kisha akatoka haraka akaenda kwenye kundi la ng'ombe, akachagua ndama mmoja mzuri na mnono, akamkabidhi mtumishi ambaye aliharakisha kumchinja na kumpika. Halafu Abrahamu akachukua siagi, maziwa na ile nyama iliyotayarishwa, akawaandalia wageni hao chakula; naye akasimama karibu nao kuwahudumia walipokuwa wakila chini ya mti. Wale wageni wakamwuliza, “Mkeo Sara yuko wapi?” Abrahamu akawajibu, “Yumo hemani.” Mmoja wao akasema, “Hakika nitakurudia wakati kama huu mwakani, na mkeo Sara atakuwa na mtoto wa kiume.” Sara alikuwa huko nyuma mlangoni mwa hema, akisikiliza. Abrahamu na Sara walikuwa wakongwe, naye Sara mambo ya kawaida ya wanawake yalikuwa yamekoma kitambo. Kwa hiyo, Sara alicheka kimoyomoyo akisema, “Mimi ni mzee, na mume wangu hali kadhalika. Je, nikiwa mzee hivi, nitaweza kufurahi na kupata watoto?” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kujiuliza kama kweli itawezekana apate mtoto akiwa mzee? Je, kuna jambo lolote lisilowezekana kwa Mwenyezi-Mungu? Nitakurudia wakati uliopangwa, wakati kama huu mwakani, na Sara atakuwa na mtoto wa kiume.” Lakini Sara, akiwa na hofu, akakana akisema, “Sikucheka!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sivyo! Kucheka, ulicheka.” Ndipo wale watu wakaondoka, wakafika mahali walipoweza kuona mji wa Sodoma; naye Abrahamu akawasindikiza. Basi, Mwenyezi-Mungu akawaza: Je, nimfiche Abrahamu jambo ambalo nimepanga kutenda? Yeye atakuwa baba wa taifa kubwa na kwake mataifa yote ya ulimwengu yatabarikiwa! Nimemchagua yeye na wazawa wake. Yeye atawafunza wazawa wake kushika njia yangu: Wawe waadilifu na wenye kutenda mambo ya haki, nami nipate kuwatimizia ahadi zangu. Basi, Mwenyezi-Mungu akasema, “Kuna malalamiko mengi dhidi ya watu wa Sodoma na Gomora, na dhambi yao ni kubwa mno. Hivyo nitashuka kwenda huko nijionee mwenyewe kama kweli wamefanya kadiri ya kilio kilichonifikia. Nataka kujua.” Kutoka hapo, wale watu wakashika njia kuelekea Sodoma, lakini Mwenyezi-Mungu akawa amebaki, amesimama pamoja na Abrahamu. Basi, Abrahamu akamkaribia Mwenyezi-Mungu, akamwuliza, “Je, kweli utawaangamiza watu wema pamoja na waovu? Huenda ikawa mna watu wema hamsini humo mjini. Je, utauangamiza mji mzima badala ya kuuacha kwa sababu ya hao wema hamsini waliomo humo? Sidhani kama utafanya hivyo! Kuwaua watu wema pamoja na waovu; wema kutendewa sawa na waovu! La, hasha! Hakimu wa dunia yote hataacha kutenda yaliyo sawa!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nikikuta watu wema hamsini kule mjini Sodoma, basi nitauacha mji wote salama kwa ajili yao.” Abrahamu akasema, “Nimethubutu kuzungumza na Bwana, mimi niliye mavumbi na majivu tu. Huenda wakapatikana watu wema arubaini na watano badala ya hamsini. Je, utauangamiza mji mzima kwa sababu wamepungua watu watano?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sitauangamiza mji ikiwa kuna watu wema arubaini na watano.” Abrahamu akaongeza kusema, “Pengine watu arubaini watapatikana humo.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa ajili ya watu wema arubaini, sitafanya hivyo.” Abrahamu akaongeza kusema, “Ee Bwana, naomba usinikasirikie, nami nitasema tena. Huenda wakapatikana watu wema thelathini.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sitafanya hivyo nikiwakuta hao thelathini.” Abrahamu akasema, “Nimethubutu kuzungumza na Bwana. Labda watapatikana watu wema ishirini.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.” Hatimaye, Abrahamu akasema, “Ee Bwana, nakuomba usikasirike, ila nitasema tena mara moja tu. Je, wakipatikana watu wema kumi, itakuwaje?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa ajili ya hao watu wema kumi, sitauangamiza mji huo.” Mwenyezi-Mungu alipomaliza kuzungumza na Abrahamu, alikwenda zake; naye Abrahamu akarudi nyumbani kwake. Wale malaika wawili wakawasili mjini Sodoma jioni. Loti ambaye alikuwa ameketi penye lango la mji wa Sodoma, alipowaona, aliinuka kuwalaki, akainama kwa heshima, akasema, “Bwana zangu, karibuni nyumbani kwangu mimi mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala kwangu usiku wa leo. Asubuhi na mapema mtaweza kuendelea na safari yenu.” Lakini, wao wakasema, “La! Sisi tutalala huku mtaani.” Loti akawasihi sana, mwishowe wakakubali, wakageuka na kuingia nyumbani kwake. Loti akawaandalia karamu, akaoka mikate isiyotiwa chachu, wakala. Lakini kabla ya kulala usiku, wanaume wote wa mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, bila kubaki hata mmoja, wakaizingira nyumba ya Loti. Wakamwita Loti na kumwuliza, “Wako wapi wale wanaume waliokuja kwako? Watoe nje. Tunataka kulala nao.” Loti akatoka nje, akafunga mlango nyuma yake, akawaambia, “Ndugu zangu, nawasihi msitende uovu huo. Tazama, ninao binti wawili ambao bado hawajalala na mwanamume. Mniruhusu niwapeni hao wasichana muwatendee kama mpendavyo. Lakini msiwatende lolote wanaume hawa kwa sababu ni wageni wangu.” Lakini wao wakasema, “Tupishe! Wewe ulikuja huku ukiwa mgeni na sasa wajifanya hakimu! Basi, tutakutenda mabaya zaidi ya hao wageni wako.” Hapo wakamsukuma Loti nyuma hata karibu wauvunje mlango wake. Lakini wale wageni wakanyosha mikono yao, wakamvuta Loti ndani ya nyumba na kuufunga mlango. Kisha wakawapiga kwa kuwapofusha macho wanaume wote waliokuwapo mlangoni, wakubwa kwa wadogo, hata wakataabika kuutafuta ule mlango, wasiupate. Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Je, una mtu mwingine hapa, pengine wana, mabinti, wachumba wa binti zako au watu wengine wa jamaa yako wanaoishi mjini humu? Watoe mahali hapa haraka, kwa maana kilio kilichomfikia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wakazi wa hapa ni kikubwa mno, naye ametutuma tuje kuwaangamiza.” Basi, Loti akawaendea wachumba wa binti zake, akawaambia, “Haraka! Tokeni mahali hapa, maana Mwenyezi-Mungu atauangamiza mji huu.” Lakini wao wakamwona kama mtu mcheshi tu. Kulipokucha, malaika wakamhimiza Loti wakisema, “Amka, mchukue mkeo na hawa binti zako wawili msije mkaangamia wakati mji huu unapoadhibiwa.” Loti akawa anasitasita. Lakini kwa vile Mwenyezi-Mungu alivyomhurumia Loti, wale malaika wakamshika yeye, mkewe na binti zake wawili, wakamtoa nje ya mji. Walipowatoa nje ya mji, malaika mmoja wao akawaambia, “Kimbieni kwa usalama wenu. Msiangalie nyuma wala kusimama popote bondeni. Kimbilieni milimani, msije mkaangamia.” Loti akawaambia, “La, bwana zangu! Ni kweli kwamba mimi mtumishi wenu nimepata fadhili mbele yenu, nanyi mmenionea huruma sana kwa kuyaokoa maisha yangu; lakini milimani ni mbali mno. Maangamizi haya yatanikuta kabla sijafika huko, nami nitakufa. Tazameni, kule kuna mji mdogo ambao naweza kuukimbilia kwani uko karibu. Basi, mniruhusu nikimbilie huko. Ule ni mji mdogo tu, na huko nitasalimika.” Naye akamjibu, “Sawa, nimekubali ombi lako. Sitauangamiza mji ulioutaja. Harakisha! Kimbilia huko, nami sitafanya lolote mpaka utakapowasili huko.” Hivyo mji huo ukaitwa Soari. Jua lilikuwa limekwisha chomoza wakati Loti alipowasili mjini Soari. Ndipo Mwenyezi-Mungu akateremsha moto mkali wa kiberiti kutoka mbinguni juu ya Sodoma na Gomora, akaiangamiza miji hiyo, bonde lote, wakazi wake wote na mimea yote katika nchi hiyo. Lakini mkewe Loti aliyekuwa nyuma ya Loti, akatazama nyuma, akageuka nguzo ya chumvi. Asubuhi na mapema, Abrahamu alikwenda mahali alipokuwa amesimama mbele ya Mwenyezi-Mungu. Akiwa hapo, akatazama chini pande za Sodoma na Gomora na eneo lote la bondeni, akashangaa kuona moshi ukipanda, moshi kama wa tanuri kubwa. Mungu alipoiangamiza miji ya bondeni alimokuwa anakaa Loti, alimkumbuka Abrahamu kwa kumtoa Loti katika miji hiyo, ili Loti asije akaangamia pamoja nayo. Loti aliogopa kuishi mjini Soari, kwa hiyo akauhama mji huo, yeye pamoja na binti zake wawili, wakaenda kuishi pangoni, milimani. Wakiwa huko, binti mkubwa akamwambia dada yake, “Baba yetu ni mzee, na hakuna mwanamume nchini wa kutuoa tupate watoto. Basi, tumlevye baba kwa divai, ili tupate kulala naye na kudumisha uzawa kwa kupata watoto kwake.” Usiku huo wakamlevya baba yao kwa divai, na yule binti wa kwanza akaenda akalala naye. Lakini baba yake hakujua wakati bintiye alipolala naye, wala alipoondoka. Kesho yake, yule binti wa kwanza akamwambia yule mdogo, “Jana usiku mimi nililala na baba; leo pia tumlevye kwa divai, kisha wewe utalala naye, na hivyo sote tutadumisha uzao kwa kupata watoto.” Basi, usiku huo pia wakamlevya baba yao kwa divai, kisha yule binti mdogo akaenda akalala naye. Lakini baba yake hakujua wakati bintiye alipolala naye, wala alipoondoka. Hivyo, binti wote wawili wa Loti wakapata mimba kutokana na baba yao. Yule binti wa kwanza akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Moabu. Huyo ndiye baba wa Wamoabu hadi leo. Yule mdogo pia akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Ben-ami. Huyo ndiye baba wa Waamoni hadi leo. Toka Mamre, Abrahamu alisafiri kuelekea eneo la Negebu, akafanya makao yake kati ya Kadeshi na Shuri, kisha akaenda kukaa kwa muda huko Gerari. Akiwa huko, Abrahamu alisema kuwa mkewe Sara ni dada yake. Kwa hiyo, mfalme Abimeleki wa Gerari akamchukua Sara. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto usiku, akamwambia, “Wewe utakufa kwa sababu ya mwanamke uliyemchukua, kwani ana mumewe.” Abimeleki ambaye bado hakuwa amelala na Sara, akajibu, “Bwana, utawaua watu wasio na hatia. Abrahamu mwenyewe ndiye aliyesema kuwa huyu ni dada yake. Tena hata Sara mwenyewe alisema kuwa Abrahamu ni kaka yake! Mimi nimefanya nilivyofanya kwa moyo mnyofu na sina hatia.” Basi, Mungu akamwambia katika hiyo ndoto, “Sawa. Najua kwamba umefanya hivyo kwa moyo mnyofu, na mimi ndiye niliyekuzuia kutenda dhambi dhidi yangu; ndiyo maana sikukuruhusu umguse huyo mwanamke. Sasa mrudishe huyo mwanamke kwa mume wake. Abrahamu ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini usipomrudisha, ujue kwa hakika kwamba wewe utakufa pamoja na watu wako wote.” Basi, Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumishi wake wote na kuwaeleza mambo aliyoyaona katika ndoto; nao wakaogopa sana. Ndipo Abimeleki akamwita Abrahamu, akamwuliza, “Umetutendea nini? Nimekukosea nini hata ukaniletea balaa hili mimi na ufalme wangu? Umenitendea mambo yasiyostahili kutendwa.” Tena Abimeleki akazidi kumwuliza, “Ni kitu gani kimekusukuma kufanya hivyo?” Abrahamu akamjibu, “Nilifanya hivyo kwa kuwa hakuna amchaye Mungu mahali hapa, na kwamba mngeniua ili mumchukue mke wangu. Zaidi ya hayo, kwa kweli, yeye ni dada yangu: Baba yake na baba yangu ni mmoja, lakini mama tofauti; ndiyo maana akawa mke wangu. Wakati Mungu aliponifanya niiache nyumba ya baba yangu na kwenda ugenini, nilimwambia mke wangu, ‘Popote tutakapokwenda tafadhali useme kwamba mimi ni kaka yako!’” Abimeleki akamrudishia Abrahamu mke wake Sara, akampa na kondoo, ng'ombe na watumwa wa kiume na kike. Tena Abimeleki akamwambia Abrahamu, “Tazama, nchi hii yote ni yangu! Basi, chagua popote upendapo, ukae.” Kisha, akamwambia Sara, “Tazama, mimi nimempa ndugu yako vipande 1,000 vya fedha ili kuwaonesha wote walio pamoja nawe kwamba huna hatia; umethibitishwa huna lawama.” Kisha Abrahamu akamwomba Mungu, naye akamponya Abimeleki, mkewe na mjakazi wake, hata wakaweza kupata tena watoto. Hapo kwanza Mwenyezi-Mungu alikuwa amewazuia wanawake wote wa nyumba ya Abimeleki kupata watoto kwa sababu ya Sara, mke wa Abrahamu. Mwenyezi-Mungu alimkumbuka Sara, akamtendea kama alivyoahidi. Basi, Abrahamu akiwa mzee, Sara akapata mimba, akamzalia mtoto wa kiume, wakati uleule Mungu alioutaja. Abrahamu akampa huyo mwanawe ambaye Sara alimzalia jina Isaka. Isaka alipotimiza umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri kama alivyoamriwa na Mungu. Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 100 wakati mwanawe Isaka alipozaliwa. Naye Sara akasema, “Mungu amenipatia kicheko; yeyote atakayesikia habari hizi, atacheka pamoja nami.” Kisha akaongeza, “Ni nani angeweza kumwambia Abrahamu kwamba mimi Sara nitanyonyesha watoto? Tena nimemzalia mtoto wa kiume katika uzee wake!” Isaka akaendelea kukua, na siku alipoachishwa kunyonya, Abrahamu akafanya sherehe kubwa. Baadaye Sara alimwona Ishmaeli, mtoto wa Abrahamu aliyezaliwa na Hagari, Mmisri, akicheza na Isaka mwanawe. Basi, Sara akamwambia Abrahamu, “Mfukuzie mbali mjakazi huyu na mwanawe. Haiwezekani kabisa mtoto wa mjakazi kurithi pamoja na mwanangu Isaka.” Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa kuwa Ishmaeli pia alikuwa mtoto wake. Lakini Mungu akamwambia Abrahamu, “Usihuzunike kwa sababu ya mtoto huyu, wala huyo mtumwa wako wa kike. Lolote akuambialo Sara lifanye; kwa kweli wazawa wako watatokana na Isaka. Na kuhusu huyo mwana wa mjakazi wako, nitamfanya awe baba wa taifa kubwa kwa kuwa yeye pia ni mtoto wako.” Hivyo, asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari na kumtwika begani; akamfukuza pamoja na mwanawe. Hagari akaondoka, akawa anatangatanga nyikani Beer-sheba. Ikawa maji yalipomwishia katika kile kiriba, Hagari akamlaza mwanawe chini ya mti. Naye akaenda kando, akaketi umbali wa kama mita 100 hivi, akisema moyoni mwake, “Heri nisimwone mwanangu akifa.” Na alipokuwa ameketi hapo, mtoto akalia kwa sauti. Mungu akamsikia mtoto huyo akilia, na malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni, akamwambia, “Una shida gani Hagari? Usiogope; Mungu amesikia sauti ya mtoto huko alipo. Simama umwinue mtoto na kumshika vizuri mikononi mwako, kwani nitamfanya awe baba wa taifa kubwa.” Mungu akamfumbua Hagari macho, naye akaona kisima cha maji. Akaenda akajaza kiriba maji, akamnywesha mtoto wake. Mungu akawa pamoja na huyo mtoto, naye akaendelea kukua. Alikaa nyikani na akawa mpiga upinde hodari sana. Alikuwa akikaa katika nyika za Parani, na mama yake akamwoza mke kutoka nchi ya Misri. Wakati huo, Abimeleki pamoja na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, alimwendea Abrahamu, akamwambia, “Mungu yuko pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. Kwa hiyo niapie kwa jina la Mungu kwamba hutanifanyia hila mimi au watoto wangu au wazawa wangu. Kadiri mimi nilivyokuwa mwaminifu kwako, vivyo hivyo nawe uwe mwaminifu kwangu na kwa nchi hii unamokaa.” Abrahamu akasema, “Naapa.” Wakati huo Abrahamu alikuwa amemlalamikia Abimeleki juu ya kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyanganya. Abimeleki akamwambia, “Mimi sijui nani aliyefanya hivyo; mpaka leo hii wewe hukuniambia; wala mimi sijapata kusikia habari hizi hadi leo.” Basi, Abrahamu akachukua kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki nao wawili wakafanya agano baina yao. Abrahamu akatenga wanakondoo wa kike saba. Abimeleki akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini unawatenga hao wanakondoo wa kike saba?” Abrahamu akamjibu, “Hawa wanakondoo wa kike saba ninakupa kwa mkono wangu mwenyewe kama shahidi wangu kwamba mimi ndimi niliyechimba kisima hiki.” Kwa hiyo kisima hicho kikaitwa Beer-sheba, maana wote wawili walikula kiapo mahali hapo. Hivyo, wakafanya agano huko Beer-sheba. Abimeleki na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, akaondoka na kurudi katika nchi ya Wafilisti. Abrahamu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akamwabudu Mungu, Mungu wa milele. Abrahamu alikaa katika nchi ya Wafilisti muda mrefu. Baada ya muda fulani, Mungu alimjaribu Abrahamu. Mungu alimwita, “Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam nasikiliza.” Mungu akamwambia, “Mchukue mwanao, Isaka, mwanao wa pekee umpendaye, uende mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuonesha.” Basi, kesho yake, Abrahamu akaamka asubuhi na mapema, akatandika punda wake, akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Akatayarisha kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kisha akaanza safari kuelekea mahali alipoambiwa na Mungu. Mnamo siku ya tatu, Abrahamu aliinua macho akapaona mahali hapo kwa mbali. Akawaambia wale watumishi wake, “Ngojeni hapa na huyu punda. Mimi na mwanangu tutakwenda mpaka kule, tukamwabudu Mungu, kisha tutawarudiani.” Basi, Abrahamu akazitwaa zile kuni, akamtwika Isaka mwanawe; yeye mwenyewe akachukua moto na kisu mkononi; wakaondoka pamoja. Isaka akamwuliza baba yake, “Baba, moto na kuni tunazo; lakini mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa yuko wapi?” Abrahamu akamjibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atatujalia mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa.” Basi, wakaendelea na safari yao. Walipofika mahali ambapo Mungu alimwagiza, Abrahamu akajenga madhabahu na kupanga kuni juu yake. Kisha akamfunga Isaka mwanawe na kumlaza juu ya kuni juu ya madhabahu. Abrahamu akaunyosha mkono wake, akatwaa kisu tayari kumchinja mwanawe. Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita kutoka mbinguni, “Abrahamu! Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam, nasikiliza!” Malaika akamwambia, “Usimdhuru mtoto wala usimfanye lolote! Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwani hukuninyima hata mwanao wa pekee.” Ndipo Abrahamu akatazama, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake kichakani. Basi, akaenda, akamchukua huyo kondoo, akamtoa sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Kwa hiyo, Abrahamu akapaita mahali hapo, “Mwenyezi-Mungu hujalia.” Kama isemwavyo hata leo, “Katika mlima wa Mwenyezi-Mungu, watu hujaliwa.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita Abrahamu mara ya pili kutoka mbinguni, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimeapa kwa nafsi yangu kwamba kwa kuwa umefanya hivi, wala hukuninyima mwanao wa pekee, hakika nitakubariki, na wazawa wako nitawazidisha kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ufuoni mwa bahari. Wazawa wako wataimiliki miji ya adui zao. Kutokana na wazawa wako mataifa yote duniani yatabarikiwa kwa sababu wewe umeitii amri yangu.” Basi, Abrahamu akawarudia wale watumishi wake, nao kwa pamoja wakaondoka, wakarudi Beer-sheba; Abrahamu akakaa huko Beer-sheba. Baada ya matukio hayo Abrahamu alipata habari kwamba Milka pia amemzalia Nahori, nduguye, watoto wa kiume: Usi mzaliwa wa kwanza, Buzi ndugu yake, Kemueli baba yake Aramu, Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli. Bethueli alimzaa Rebeka. Milka alimzalia Nahori, ndugu yake Abrahamu, watoto hao wanane. Zaidi ya hayo, Reuma, suria wa Nahori, pia alimzalia watoto: Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka. Sara aliishi miaka 127. Hiyo ndiyo iliyokuwa miaka ya maisha yake Sara. Alifia huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Abrahamu akaomboleza na kumfanyia matanga Sara mkewe. Abrahamu akaiacha maiti ya mkewe, akatoka kwenda kuzungumza na Wahiti, akawaambia, “Mimi ninaishi kama mgeni miongoni mwenu. Nipatieni sehemu ya ardhi ya kaburi, ili nipate kumzika marehemu mke wangu.” Wahiti wakamjibu, “Ee bwana wetu, tusikilize; wewe ni kiongozi maarufu miongoni mwetu. Mzike marehemu mkeo katika kaburi lolote utakalojichagulia; hakuna yeyote miongoni mwetu atakayekunyima kaburi lake, wala kukuzuia kumzika marehemu mkeo.” Hapo Abrahamu akasimama na kuinama kwa heshima mbele ya wananchi Wahiti, akawaambia, “Ikiwa mnaniruhusu nimzike marehemu mke wangu, tafadhali mwombeni Efroni mwana wa Sohari, kwa niaba yangu, aniuzie lile pango lake la Makpela lililo mpakani mwa shamba lake. Msihini aniuzie nilifanye makaburi yangu; anipatie kwa bei ya haki papa hapa mbele yenu.” Efroni mwenyewe alikuwa miongoni mwa Wahiti hao waliokuwa wamekutanika penye lango la mji. Basi, Efroni Mhiti, akamjibu Abrahamu, mbele ya Wahiti wote hapo langoni, “La, bwana; tafadhali unisikilize. Ninakupa shamba lote na pango lililomo humo; tena ninakupa mbele ya wananchi wenzangu. Mzike humo marehemu mkeo.” Abrahamu akainama tena kwa heshima mbele ya wananchi, akamwambia Efroni, wananchi wote wakisikia, “Nakuomba, tafadhali unisikilize. Nitakulipa bei kamili ya shamba lako, na ninakuomba upokee malipo haya, ili nipate kumzika humo marehemu mke wangu.” Efroni akamjibu Abrahamu, “Bwana, nisikilize; shamba lenye thamani ya shekeli 400 tu za fedha ni nini kati yako na mimi? Mzike marehemu mke wako.” Abrahamu akakubaliana na Efroni, akampimia kiasi cha fedha alichotaja mbele ya Wahiti wote, fedha shekeli 400, kadiri ya vipimo vya wafanyabiashara wa wakati huo. Basi, shamba la Efroni lililoko huko Makpela, mashariki ya Mamre, pango na miti yote iliyokuwamo pamoja na eneo zima, likawa lake Abrahamu mbele ya Wahiti wote waliokutanika penye lango la mji. Baada ya hayo, Abrahamu akamzika Sara mkewe katika pango hilo lililokuwamo katika shamba la Makpela, mashariki ya Mamre (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani. Shamba na pango lililokuwamo humo lilithibitishwa na Wahiti liwe mali yake Abrahamu apate kuzika humo wafu wake. Sasa Abrahamu alikuwa mzee wa miaka mingi, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa amembariki katika kila hali. Siku moja Abrahamu akamwambia mtumishi wake aliyekuwa mzee kuliko wengine na msimamizi wa mali yake yote, “Weka mkono wako mapajani mwangu, nami nitakuapisha kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu na dunia, kwamba hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ninaoishi nao. Niapie kwamba utakwenda mpaka katika nchi yangu, kwa jamaa zangu, umtafutie mwanangu Isaka mke.” Mtumishi akamwambia, “Huenda mwanamke huyo atakataa kufuatana nami kuja huku, ikiwa hivyo, je, ni lazima nimrudishe mwanao nchini ulikotoka?” Abrahamu akamwambia, “La! Angalia sana usimrudishe mwanangu huko. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani kwa baba yangu na kutoka katika nchi nilimozaliwa, na ambaye alisema nami, aliniapia kwamba atawapa wazawa wangu nchi hii. Yeye atamtuma malaika wake mbele yako ili umletee mwanangu mke kutoka huko. Iwapo mwanamke huyo hatapenda kufuatana nawe hadi huku, basi kiapo changu hakitakufunga, lakini kwa vyovyote vile usimrudishe mwanangu huko.” Basi, mtumishi huyo akaweka mkono wake mapajani mwa Abrahamu, bwana wake, akaapa kuhusu jambo hilo. Kisha, huyo mtumishi akachukua ngamia kumi wa bwana wake akaondoka akiwa na zawadi nzuri za kila aina. Akasafiri kwenda katika mji alimokaa Nahori, nchini Mesopotamia. Alipowasili, aliwapigisha magoti ngamia wake kando ya kisima kilichokuwa nje ya mji. Ilikuwa jioni wakati ambapo wanawake huenda kisimani kuteka maji. Naye akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba unijalie nifaulu leo na umfadhili Abrahamu bwana wangu. Niko hapa kando ya kisima ambapo binti za wenyeji wa mji huja kuteka maji. Basi, msichana nitakayemwambia atue mtungi wake wa maji anipatie maji ninywe, naye akanipa mimi pamoja na kuwanywesha ngamia wangu, na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka. Jambo hilo litanionesha kwamba umemfadhili bwana wangu.” Kabla hajamaliza kuomba, mara Rebeka, binti Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu yake Abrahamu, akafika amebeba mtungi wake begani. Msichana huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, na bikira ambaye hakuwa amelala na mwanamume yeyote. Basi, akateremka kisimani, akaujaza mtungi wake maji na kupanda. Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye, akamwambia, “Tafadhali, nipatie maji ya kunywa kutoka mtungi wako.” Msichana akamjibu, “Haya kunywa bwana wangu.” Na papo hapo akautua mtungi wake, akiushikilia ili amnyweshe. Alipokwisha kumpatia maji, akamwambia, “Nitawatekea maji ngamia wako pia, wanywe mpaka watosheke.” Basi, akafanya haraka, akawamiminia ngamia maji ya mtungi wake katika hori, akakimbia kisimani kuteka maji mengine na kuwanywesha ngamia wake wote. Yule mtu akawa anamtazama kwa makini bila kusema lolote, apate kufahamu kama Mwenyezi-Mungu ameifanikisha safari yake au sivyo. Ngamia walipotosheka kunywa maji, yule mtu akampa huyo msichana pete ya dhahabu yenye uzito upatao gramu sita, na bangili mbili za dhahabu za gramu kumi kila moja. Akamwuliza, “Niambie tafadhali: Wewe ni binti nani? Je, kuna nafasi ya kulala nyumbani kwenu?” Rebeka akajibu, “Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori. Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha na mahali pa kulala wageni.” Ndipo yule mtu akainamisha kichwa chake, akamwabudu Mwenyezi-Mungu akisema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hajasahau fadhili zake na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mwenyezi-Mungu ameniongoza mimi mwenyewe moja kwa moja hadi kwa jamaa ya bwana wangu!” Kisha yule msichana akakimbia kwenda kuwapa habari jamaa za mama yake. Rebeka alikuwa na kaka yake aitwaye Labani. Labani akatoka mbio kukutana na yule mtu kisimani. Labani alikuwa ameiona ile pete na bangili mikononi mwa dada yake, na kusikia mambo Rebeka aliyoambiwa na huyo mtu. Labani alimkuta yule mtu amesimama karibu na ngamia wake kando ya kisima. Labani akamwambia, “Karibu kwetu wewe uliyebarikiwa na Mwenyezi-Mungu. Mbona unasimama nje? Mimi mwenyewe nimekwisha tayarisha nyumba na mahali kwa ajili ya hawa ngamia wako!” Basi, mtumishi huyo wa Abrahamu akaingia nyumbani. Labani akawafungua ngamia na kuwapatia majani ngamia wake, akampa yeye na watu wake maji ya kunawa miguu. Basi, wakamwandalia chakula, lakini yeye akasema, “Sitakula mpaka nimesema ninachotaka kusema.” Labani akamwambia, “Haya, tuambie.” Yule mtu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu. Mwenyezi-Mungu amembariki sana bwana wangu, naye amekuwa mtu maarufu. Amempa makundi ya kondoo na mifugo mingi, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda! Sara, mke wa bwana wangu katika uzee wake, alimzalia bwana wangu mtoto; na bwana wangu amempa huyo mtoto mali yake yote. Bwana wangu aliniapisha mimi akisema, ‘Hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ambao ninaishi katika nchi yao. Bali utakwenda mpaka nchi yangu, kwa jamaa zangu, ili umtafutie mwanangu Isaka mke.’ Nami nikamwambia bwana wangu, ‘Huenda mwanamke huyo akakataa kufuatana nami kuja huku.’ Lakini yeye akasema, ‘Mwenyezi-Mungu aniongozaye maishani mwangu, atamtuma malaika wake aende pamoja nawe na kukufanikisha katika safari yako; nawe utamtwalia mwanangu mke kutoka kwa jamaa yangu na nyumba ya baba yangu. Kama utakapofika kwa jamaa zangu hawatakupa huyo msichana, basi, hutafungwa na kiapo changu.’ “Leo nilipofika kisimani nimeomba, ‘Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba nifaulu leo katika safari yangu na umfadhili Abrahamu bwana wangu. Niko hapa kando ya kisima. Msichana atakayekuja kuteka maji ambaye nitamwomba anipatie maji kidogo ya kunywa kutoka mtungi wake, naye akanipa na kuwatekea maji ngamia wangu, basi huyo na awe ndiye uliyemchagua kuwa mke wa mwana wa bwana wangu.’ “Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, mara Rebeka alifika na mtungi wake wa maji begani, akateremka kisimani na kuteka maji. Nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ya kunywa.’ Naye akautua mtungi wake haraka kutoka begani mwake, akasema, ‘Haya, kunywa bwana wangu. Nitawatekea maji ngamia wako pia.’ Basi mimi nikanywa na ngamia wangu pia akawapa maji. Ndipo nilipomwuliza, ‘Je, wewe ni binti wa nani?’ Akaniambia, ‘Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori.’ Ndipo nilipompa pete na kumvisha bangili mikononi. Kisha nikainama na kumwabudu Mwenyezi-Mungu; nikamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye ameniongoza moja kwa moja kwa binti wa ukoo wa bwana wangu kwa ajili ya mwanawe. Sasa, basi, niambieni kama mko tayari kumtendea bwana wangu kwa uaminifu na haki; kama sivyo, basi semeni, nami nitajua cha kufanya.” Baada ya kusikia hayo, Labani na Bethueli wakamjibu, “Jambo hili limetoka kwa Mwenyezi-Mungu, sisi hatuwezi kuamua lolote. Rebeka huyu hapa; mchukue uende. Na awe mke wa mwana wa bwana wako kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.” Mtumishi wa Abrahamu aliposikia maneno hayo, alimsujudia Mwenyezi-Mungu. Kisha akatoa vito vya fedha na dhahabu na nguo, akampa Rebeka. Pia aliwapa ndugu na mama yake Rebeka mapambo ya thamani kubwa. Mtumishi wa Abrahamu na watu aliokuja nao wakala, wakanywa na kulala huko. Walipoamka asubuhi, mtumishi yule akasema, “Naomba kurudi kwa bwana wangu.” Lakini ndugu na mama yake Rebeka wakasema, “Mwache msichana akae nasi muda mfupi, kama siku kumi hivi; kisha anaweza kwenda.” Lakini yeye akasema, “Tafadhali, msinicheleweshe, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha fanikisha safari yangu; naomba mniruhusu kurudi kwa bwana wangu.” Nao wakasema, “Basi, tumwite msichana mwenyewe, tumwulize.” Wakamwita Rebeka na kumwuliza, “Je, utakwenda na mtu huyu?” Naye akajibu, “Nitakwenda.” Basi, wakamwacha Rebeka na yaya wake aende na mtumishi wa Abrahamu na watu wake. Yaya wake Rebeka pia aliandamana naye. Basi, wakambariki Rebeka wakisema, “Ewe dada yetu! Uwe mama wa maelfu kwa maelfu; wazawa wako waimiliki miji ya adui zao.” Kisha, Rebeka na wajakazi wake wakapanda ngamia na kumfuata huyo mtumishi wa Abrahamu; nao wote wakaondoka. Wakati huo, Isaka alikuwa ameondoka Beer-lahai-roi, akawa anakaa huko pande za Negebu. Siku moja jioni, Isaka alikwenda mashambani kutafakari. Basi, akatazama akaona ngamia wanakuja. Naye Rebeka alipotazama na kumwona Isaka, alishuka chini na kumwuliza mtumishi wa Abrahamu, “Ni nani yule mtu anayetembea kule shambani, anakuja kutulaki?” Yule mtumishi akasema, “Ni bwana wangu.” Basi, Rebeka akatwaa shela yake, akajifunika uso. Yule mtumishi akamsimulia Isaka yote aliyokuwa ameyafanya. Basi, Isaka akamchukua Rebeka ndani ya hema iliyokuwa ya Sara mama yake, akawa mke wake. Isaka akampenda Rebeka na kupata faraja baada ya kifo cha mama yake. Abrahamu alioa mke mwingine, jina lake Ketura. Ketura alimzalia Abrahamu: Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua. Yokshani alimzaa Sheba na Dedani; wazawa wa Dedani walikuwa Waashuru, Waletushi na Waleumi. Watoto wa Midiani walikuwa Efa, Eferi, Henoki, Abida na Eldaa. Wote hao walikuwa wazawa wa Ketura. Abrahamu alimrithisha Isaka mali yake yote. Lakini watoto wa kiume wa masuria wake akawapa zawadi, na wakati alipokuwa bado hai, aliwapeleka katika nchi ya mashariki, mbali na Isaka mwanawe. Abrahamu aliishi miaka 175. Alifariki baada ya kuishi maisha marefu na ya fanaka, akajiunga na wazee wake waliomtangulia. Isaka na Ishmaeli, wanawe Abrahamu, wakamzika baba yao katika pango la Makpela, mashariki ya Mamre kwenye shamba lililokuwa la Efroni, mwana wa Sohari, Mhiti. Abrahamu alikuwa amenunua shamba hilo kwa Wahiti. Huko ndiko alikozikwa Abrahamu na mkewe Sara. Baada ya kifo cha Abrahamu, Mungu alimbariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akawa anaishi karibu na kisima cha Beer-lahai-roi. Hawa ndio wazawa wa Ishmaeli mwanawe Abrahamu ambaye Hagari Mmisri, aliyekuwa mjakazi wa Sara, alimzalia Abrahamu. Hii ni orodha yao kufuatana na kuzaliwa kwao: Nebayothi, mzaliwa wa kwanza, Kedari, Adbeeli, Mibsamu, Mishma, Duma, Masa, Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi na Kedema. Hao ndio watoto wa kiume wa Ishmaeli, waliokuwa asili ya makabila kumi na mawili; makazi na vijiji vyao vilijulikana kwa majina yao. Ishmaeli alikuwa na umri wa miaka 137 alipofariki, akajiunga na wazee wake waliotangulia. Wazawa wa Ishmaeli walikaa katika eneo lililo kati ya Hawila na Shuri, mashariki ya Misri, kuelekea Ashuru. Walikaa kwa utengano na wazawa wengine wa Abrahamu. Hawa ndio wazawa wa Isaka mwana wa Abrahamu. Isaka alipokuwa na umri wa miaka arubaini alimwoa Rebeka, binti Bethueli, Mwaramu wa Padan-aramu. Rebeka alikuwa dada yake Labani. Rebeka alikuwa tasa, kwa hiyo Isaka akamwomba Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu akakubali ombi lake, Rebeka akapata mimba. Mimba hiyo ilikuwa ya mapacha. Watoto hao wakashindana tumboni mwake Rebeka, naye akasema, “Kama hivi ndivyo mambo yalivyo, ya nini kuishi?” Basi, akaenda kumwuliza Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako; makabila mawili yatakayozaliwa nawe, yatafarakana. Moja litakuwa lenye nguvu kuliko lingine; mkubwa atamtumikia mdogo.” Siku zake za kujifungua zilipotimia, Rebeka alijifungua mapacha. Wa kwanza alikuwa mwekundu, mwenye nywele mwili wote; hivyo wakamwita Esau. Wa pili alizaliwa akiwa amemshika Esau kisigino, hivyo wakampa jina Yakobo. Isaka alikuwa na umri wa miaka sitini wakati Esau na Yakobo walipozaliwa. Watoto hao wakakua; Esau akawa mwindaji hodari, mpenda maisha ya mbugani, na Yakobo akawa mtu mtulivu, mpenda maisha ya nyumbani. Basi, Isaka akampenda Esau kwa sababu alipenda kula mawindo yake, lakini Rebeka akampenda Yakobo. Siku moja, Yakobo alipokuwa anapika dengu, Esau alirudi nyumbani kutoka mawindoni ana njaa sana. Kwa hiyo akamwambia Yakobo, “Nafa njaa; tafadhali, nigawie chakula hicho chekundu nile.” (Ndiyo maana walimpanga jina Edomu yaani mwekundu). Yakobo akajibu, “Kwanza niuzie haki yako ya mzaliwa wa kwanza.” Esau akasema, “Sawa! Niko karibu kufa; haki yangu ya mzaliwa wa kwanza itanifaa nini?” Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Basi, Esau akamwapia na kumwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na dengu kiasi. Esau akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo ndivyo Esau alivyoidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Baadaye palitokea njaa nchini humo, njaa tofauti na ile ya hapo awali wakati wa uhai wa Abrahamu. Isaka akaenda Gerari kwa Abimeleki mfalme wa Wafilisti. Mwenyezi-Mungu akamtokea Isaka na kumwambia, “Usiende Misri, bali kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa nawe na kukubariki. Nitatimiza ahadi niliyompa baba yako Abrahamu, kwani nitakupa wewe na wazawa wako nchi hizi zote. Nitawazidisha wazawa wako wawe kama nyota za mbinguni na kuwapa nchi hizi zote. Kutokana na wazawa wako, mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu Abrahamu alinitii mimi, akazingatia maagizo yangu, amri zangu, masharti yangu na sheria zangu.” Basi, Isaka akakaa huko Gerari. Watu wa huko walipomwuliza habari za mkewe, yeye alijibu, “Huyu ni dada yangu.” Aliogopa kusema kwamba ni mke wake kwa kuogopa kwamba wakazi wa nchi wangemuua kwa sababu ya Rebeka, maana Rebeka alikuwa mzuri sana. Baada ya kukaa huko kwa muda mrefu, Abimeleki mfalme wa Wafilisti alichungulia dirishani akamwona Isaka akimkumbatia mkewe Rebeka. Abimeleki akamwita Isaka na kumwambia, “Kumbe huyo ni mke wako! Mbona ulisema ni dada yako?” Isaka akajibu, “Kwa kuwa niliogopa kwamba ningeuawa kwa sababu yake.” Abimeleki akamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilotutendea? Mmoja wa watu wangu angaliweza kulala na mkeo bila wasiwasi, nawe ungekuwa umetutia hatiani.” Ndipo Abimeleki akawaonya watu wote akisema, “Yeyote atakayemgusa mtu huyu au mke wake, atauawa.” Mwaka huo Isaka alipanda mbegu katika nchi ile, akavuna mara mia zaidi, maana Mwenyezi-Mungu alimbariki, naye akatajirika. Alizidi kupata mali hadi akawa tajiri sana. Alikuwa na makundi ya kondoo, ng'ombe na watumwa wengi, hata Wafilisti wakamwonea wivu. Wafilisti walikuwa wamevifukia visima vyote vya maji ambavyo watumishi wa Abrahamu, baba yake, walikuwa wamechimba wakati alipokuwa bado hai. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwani wewe umetuzidi nguvu.” Basi, Isaka akaondoka huko, akapiga kambi yake katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akavichimbua vile visima vilivyokuwa vimechimbwa wakati Abrahamu baba yake alipokuwa hai, visima ambavyo Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kifo cha Abrahamu. Akavipa majina yaleyale aliyovipa baba yake. Lakini watumishi wa Isaka walipochimba katika lile bonde na kupata kisima cha maji yanayobubujika, wachungaji wa hapo Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu.” Hivyo Isaka akakiita kisima hicho Eseki, kwa sababu waligombana naye. Halafu wakachimba kisima kingine, nacho pia wakakigombania; hivyo Isaka akakiita kisima hicho Sitna. Kisha Isaka akaenda mahali pengine na kuchimba kisima kingine. Lakini hicho hawakukigombania; hivyo Isaka akakiita Rehobothi akisema, “Sasa Mwenyezi-Mungu ametuachia nafasi, nasi tutastawi katika nchi hii.” Kutoka huko, Isaka alikwenda Beer-sheba. Usiku huohuo Mwenyezi-Mungu alimtokea na kumwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako Abrahamu. Usiogope kwa kuwa niko pamoja nawe; nitakubariki na kuwazidisha wazawa wako kwa ajili ya Abrahamu, mtumishi wangu.” Kwa hiyo, Isaka akajenga huko madhabahu, akamwabudu Mwenyezi-Mungu. Akapiga kambi huko; na watumishi wake wakachimba kisima. Abimeleki alitoka Gerari akiwa pamoja na Ahuzathi, mshauri wake, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, akamwendea Isaka. Isaka akawauliza, “Kwa nini mmekuja kwangu hali mnanichukia na mlinifukuza kwenu?” Wao wakamjibu, “Tumeona wazi kwamba Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nawe. Kwa hiyo, tunafikiri inafaa tule kiapo pamoja nawe na kufanya agano, kwamba hutatudhuru, nasi kadhalika hatutakudhuru. Tulikutendea mema, tukakuacha uende zako kwa amani, bila kukutendea baya lolote lile. Na sasa wewe ni mbarikiwa wa Mwenyezi-Mungu.” Basi, Isaka akawafanyia karamu, nao wakala na kunywa. Kesho yake wakaamka asubuhi na mapema na kula kiapo. Kisha Isaka akawasindikiza na kuagana nao kwa amani. Siku ileile watumishi wa Isaka walimjia na kumpasha habari za kile kisima walichokuwa wamechimba, wakasema, “Tumepata maji!” Basi, Isaka akakiita kisima hicho Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba hata leo. Esau alipokuwa na umri wa miaka arubaini, alioa wake wawili Wahiti: Yudithi bintiye Beeri, na Basemathi bintiye Eloni. Wanawake hao waliyafanya maisha ya Isaka na Rebeka kuwa machungu. Isaka alikuwa amezeeka na macho yake yalikuwa hayaoni. Basi, alimwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu!” Naye akaitika “Naam baba, nasikiliza!” Isaka akasema, “Tazama, mimi ni mzee, wala siku ya kufa kwangu siijui. Basi, chukua silaha zako, yaani podo na upinde wako, uende porini ukaniwindie mnyama. Halafu unitengenezee chakula kitamu, kile nipendacho, uniletee ili nile, nipate kukubariki kabla ya kufa kwangu.” Kumbe, wakati huo Isaka alipokuwa akiongea na Esau mwanawe, Rebeka alikuwa anasikiliza. Kwa hiyo, Esau alipokwenda porini kuwinda, Rebeka alimwambia mwanawe Yakobo, “Nimemsikia baba yako akimwambia kaka yako Esau, amwindie mnyama na kumtengenezea chakula kitamu, ili ale, apate kumbariki mbele ya Mwenyezi-Mungu kabla ya kufa kwake. Sasa mwanangu, sikiliza maneno yangu na utii ninayokuagiza. Nenda kwenye kundi la mbuzi uniletee wanambuzi wawili wazuri, nimtengenezee baba yako chakula kitamu, kile apendacho. Kisha utampelekea baba yako ale, apate kukubariki kabla hajafa.” Lakini Yakobo akamwambia mama yake Rebeka, “Kumbuka kaka yangu Esau amejaa nywele mwilini, hali mimi sina. Labda baba atataka kunipapasa, nami nitaonekana kama ninamdhihaki, kwa hiyo nitajiletea laana badala ya baraka.” Mama yake akamwambia, “Laana yako na inipate mimi, mwanangu; wewe fanya ninavyokuagiza: Nenda ukaniletee hao wanambuzi.” Basi, Yakobo akaenda, akachukua wanambuzi wawili, akamletea mama yake; naye akatayarisha chakula kitamu, kile apendacho Isaka baba yake. Kisha Rebeka akatwaa mavazi bora ya Esau, mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo, mwanawe mdogo. Akamvika pia ngozi za wale wanambuzi mikononi na kwenye sehemu laini shingoni mwake. Kisha akampa kile chakula kitamu na mkate aliokuwa ametayarisha. Basi, Yakobo akaingia ndani kwa baba yake, akamwita, “Baba!” Naye akaitika, “Naam! Ni nani wewe mwanangu?” Yakobo akamjibu baba yake, “Ni mimi Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniagiza. Tafadhali baba, kaa kitako ule mawindo yangu ili upate kunibariki.” Lakini Isaka akamwuliza, “Imekuwaje umepata mawindo upesi hivyo, mwanangu?” Yakobo akamjibu, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.” Ndipo Isaka akamwambia Yakobo, “Basi, mwanangu, karibia nipate kukupapasa ili nijue kweli kama wewe ndiwe mwanangu Esau au la.” Yakobo akamkaribia baba yake Isaka, naye akampapasa na kusema, “Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.” Hakumtambua kwa sababu mikono yake ilikuwa yenye nywele nyingi kama ya Esau kaka yake; kwa hiyo akambariki. Akamwuliza tena, “Kweli wewe ndiwe mwanangu Esau?” Naye akamjibu, “Ndiyo.” Basi, baba yake akasema, “Niletee hiyo nyama nile mawindo yako mwanangu, nikubariki.” Hapo Yakobo akampelekea chakula, naye akala; akampelekea divai pia, akanywa. Ndipo baba yake Isaka, akamwambia, “Sogea karibu, mwanangu, unibusu.” Basi, Yakobo akamkaribia baba yake na kumbusu, na baba yake aliposikia harufu ya mavazi yake, akambariki akisema, “Tazama, harufu nzuri ya mwanangu ni kama harufu ya shamba alilobariki Mwenyezi-Mungu! Mungu akumiminie umande wa mbinguni; akupe ardhi yenye rutuba, nafaka na divai kwa wingi. Jamii za watu zikutumikie, na mataifa yakuinamie kwa heshima. Uwe mtawala wa ndugu zako, watoto wa kiume wa mama yako wakuinamie kwa heshima. Kila akulaaniye na alaaniwe, kila akubarikiye na abarikiwe!” Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, naye Yakobo alipokuwa ndio tu ametoka mbele ya baba yake Isaka, Esau kaka yake Yakobo, akarudi kutoka mawindoni. Esau pia akatengeneza chakula kitamu, akampelekea baba yake, akamwambia, “Haya baba, inuka ule mawindo yangu mimi mwanao, ili upate kunibariki!” Isaka akauliza, “Wewe ni nani?” Naye akamjibu, “Ni mimi mwanao Esau, mzaliwa wako wa kwanza.” Hapo Isaka akatetemeka mno, akasema, “Ni nani basi yule aliyewinda na kuniletea mawindo, nami nimekwisha kula kabla hujaja? Tena nimekwisha mbariki; naam, amekwisha barikiwa!” Esau alipoyasikia maneno ya baba yake, akaangua kilio cha uchungu. Kisha akamwambia baba yake, “Ee baba yangu, nibariki na mimi, tafadhali!” Lakini Isaka akasema, “Ndugu yako alikuja kwa hila, naye amechukua baraka yako.” Esau akasema, “Ndio maana anaitwa Yakobo! Amechukua nafasi yangu mara mbili. Kwanza alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua baraka Zangu.” Kisha akamwuliza baba yake, “Je, hukunibakizia baraka yoyote?” Isaka akamjibu, “Nimekwisha mfanya Yakobo kuwa mtawala wako, na kumpa ndugu zake wote kuwa watumishi wake. Nimempatia nafaka na divai. Nikufanyie nini sasa, wewe mwanangu?” Esau akamwambia baba yake, “Baba, kwani una baraka moja tu? Nibariki hata mimi, ee baba!” Hapo Esau akalia kwa sauti kubwa. Ndipo Isaka, baba yake, akamwambia, “Makao yako yatakuwa mbali na ardhi yenye rutuba, na mbali na umande wa mbinguni. Utaishi kwa upanga wako, na utamtumikia ndugu yako; lakini utakapoasi utaivunja kongwa yake shingoni mwako.” Basi, Esau akamchukia Yakobo kwa sababu ya baraka aliyokuwa amepewa na baba yake. Esau akawaza, “Siku za matanga ya baba zitakapokwisha, ndipo nitakapomuua ndugu yangu Yakobo.” Lakini Rebeka alipojua nia ya mwanawe mkubwa, akamwita mwanawe mdogo Yakobo, akamwambia, “Jihadhari, ndugu yako Esau anajifariji kwa kupanga kukuua. Kwa hiyo, mwanangu, sikiliza maneno yangu. Ondoka ukimbilie kwa kaka yangu Labani kule Harani. Kaa naye kwa muda, mpaka ghadhabu ya nduguyo itakapopoa. Ghadhabu yake itakapopoa, naye atakapokuwa amesahau uliyomtendea, nitatuma mtu akurudishe. Kwa nini nifiwe na nyinyi wote wawili siku moja?” Rebeka akamwambia Isaka, “Sina raha kabisa maishani kwa sababu ya hawa wanawake wa Esau Wahiti. Ikiwa Yakobo ataoa mmojawapo wa wanawake hawa Wahiti, maisha yangu yana faida gani?” Hivyo Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akisema, “Usioe mwanamke yeyote Mkanaani. Nenda Padan-aramu, nyumbani kwa babu yako Bethueli, ukaoe mmojawapo wa binti za mjomba wako Labani. Mungu mwenye nguvu na akubariki upate wazawa wengi na kuongezeka, ili uwe jamii kubwa ya watu. Akubariki wewe pamoja na wazawa wako kama alivyombariki Abrahamu, upate kuimiliki nchi ambamo unakaa kama mgeni; nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu!” Basi, Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mwaramu, kaka yake Rebeka, mama yao Yakobo na Esau. Esau alitambua kwamba Isaka alikuwa amembariki Yakobo na kumtuma aende kuoa huko Padan-aramu, na ya kuwa alipombariki, alimkataza asioe mwanamke Mkanaani. Alitambua pia kuwa Yakobo alimtii mama yake na baba yake, akaenda Padan-aramu. Basi, Esau akafahamu kwamba baba yake hapendezwi na wanawake wa Kanaani. Hivyo, mbali na wale wake zake wengine, Esau akaenda kwa Ishmaeli, mwana wa Abrahamu, akamwoa Mahalathi binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi. Yakobo aliondoka Beer-sheba, akaelekea Harani. Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Alichukua jiwe moja la mahali hapo, akaliweka chini ya kichwa chake, akalala. Aliota ndoto, na katika ndoto hiyo, aliona ngazi iliyosimamishwa duniani na ncha yake inafika mbinguni. Malaika wa Mungu walikuwa wakipanda na kushuka katika ngazi hiyo. Mwenyezi-Mungu alisimama juu ya ngazi hiyo, akamwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu baba yako, na Mungu wa Isaka. Nchi unayoilalia nitakupa wewe na wazawa wako. Wazawa wako watakuwa wengi kama mavumbi ya dunia, na milki yao itaenea kila mahali: Magharibi, Mashariki, Kaskazini na Kusini. Kwako jamii zote duniani zitabarikiwa. Mimi nipo pamoja nawe; nitakulinda popote uendapo na kukurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapotimiza ahadi niliyokupa.” Ndipo Yakobo akaamka usingizini, akasema, “Hakika, Mwenyezi-Mungu yupo mahali hapa, nami sikujua!” Yakobo akaogopa na kusema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ni nyumba ya Mungu na lango la mbinguni.” Yakobo akaamka asubuhi na mapema, akachukua lile jiwe alilokuwa ameliweka chini ya kichwa chake, akalisimika kama nguzo na kuliweka wakfu kwa kulimiminia mafuta. Akapaita mahali hapo Betheli; lakini jina la awali la mji huo lilikuwa Luzu. Kisha Yakobo akaweka nadhiri akisema, “Iwapo, ee Mungu, utakuwa pamoja nami na kunilinda katika safari yangu, ukinipa chakula na mavazi ili nirudi nyumbani kwa baba yangu salama, basi, wewe Mwenyezi-Mungu utakuwa ndiwe Mungu wangu. Nalo jiwe hili nililosimika hapa kama nguzo, litakuwa nyumba yako Mungu, nami nitakupa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote utakavyonipa.” Yakobo aliendelea na safari yake, akafika katika nchi za watu wa mashariki. Siku moja akaona kisima mbugani, na kando yake makundi matatu ya kondoo wamepumzika. Kondoo walikuwa wananyweshwa kutoka kisima hicho kilichokuwa kimefunikwa kwa jiwe kubwa. Kwa kawaida, makundi yote ya kondoo yalipokusanyika, wachungaji walivingirisha hilo jiwe kwa pamoja toka kisimani na kuwanywesha kondoo. Halafu walikifunika tena kisima kwa jiwe hilo. Yakobo akawauliza wachungaji, “Ndugu zangu, mmetoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka Harani.” Naye akawauliza, “Je, mnamfahamu Labani mwana wa Nahori?” Wakamjibu, “Tunamfahamu.” Akaendelea kuwauliza, “Je, hajambo?” Nao wakamjibu, “Hajambo; hata binti yake Raheli, yule kule anakuja na kondoo wake!” Hapo Yakobo akawaambia, “Naona bado ni mchana, na si wakati wa kuwakusanya kondoo pamoja. Basi, wanywesheni kondoo maji, mwende mkawachunge.” Lakini wao wakamwambia, “Hatuwezi kufanya hivyo mpaka makundi yote yawe yamekusanyika pamoja, na jiwe limevingirishwa kisimani, ndipo tuwanyweshe kondoo.” Yakobo alipokuwa bado anazungumza na hao wachungaji, Raheli akafika na kondoo wa baba yake, kwani ndiye aliyekuwa akiwachunga. Yakobo alipomwona Raheli, bintiye Labani, kaka ya mama yake, na alipowaona kondoo wa Labani, mjomba wake, akaenda na kulivingirisha lile jiwe kwenye mdomo wa kisima, akalinywesha maji kundi la Labani, mjomba wake. Kisha Yakobo akambusu Raheli na kulia kwa sauti. Halafu Yakobo akamjulisha Raheli kuwa yeye ni wa jamaa ya baba yake, na kwamba ni mwana wa Rebeka. Raheli akapiga mbio nyumbani akamwarifu baba yake. Labani aliposikia habari za Yakobo, mpwa wake, alikwenda mbio kumlaki, akamkumbatia, akambusu, akamkaribisha nyumbani kwake. Yakobo akamsimulia Labani mambo yote yaliyotokea. Naye Labani akasema, “Hakika, wewe ni jamaa yangu, damu moja nami!” Yakobo akakaa naye kwa muda wa mwezi mmoja. Siku moja Labani alimwambia Yakobo, “Wewe ni jamaa yangu lakini hiyo haimaanishi kwamba utanitumikia bure. Niambie unataka ujira kiasi gani!” Sasa, Labani alikuwa na binti wawili: Mkubwa aliitwa Lea, na mdogo aliitwa Raheli. Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo na wa kupendeza. Yakobo alimpenda Raheli; kwa hiyo akamwambia Labani, “Nitakutumikia miaka saba ili unioze Raheli, binti yako mdogo.” Labani akamwambia, “Afadhali nimwoze Raheli kwako wewe kuliko kumwoza mtu mwingine yeyote. Endelea kuishi nami.” Basi, Yakobo akamtumikia Labani miaka saba kwa ajili ya Raheli, lakini kwake muda huo ulikuwa kama siku chache, kwa vile alivyompenda Raheli. Kisha Yakobo akamwambia Labani, “Muda wangu umetimia, kwa hiyo nipe mke wangu.” Basi, Labani akaandaa karamu na kuwaalika watu wote wa huko. Lakini jioni, Labani akamchukua Lea, binti yake mkubwa, na kumpeleka kwa Yakobo. Yakobo akalala naye. (Labani akamtoa Zilpa, mjakazi wake, awe mtumishi wa Lea.) Asubuhi, Yakobo akagundua ya kuwa ni Lea! Basi, akamwuliza Labani, “Umenitendea jambo gani? Je, si nilikutumikia kwa ajili ya Raheli? Mbona basi, umenidanganya?” Labani akamjibu, “Nchini mwetu hatufanyi hivyo; si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya mkubwa. Mtimizie Lea siku zake saba, nasi tutakupa Raheli kwa utumishi wa miaka saba mingine.” Yakobo akakubali. Na Yakobo alipomtimizia Lea siku zake saba, Labani akampa Raheli, binti yake mdogo awe mke wake. (Labani akamtoa Bilha, mjakazi wake, awe mtumishi wa Raheli). Basi, Yakobo akalala na Raheli pia. Lakini Yakobo akampenda Raheli kuliko Lea; akamtumikia Labani miaka mingine saba. Mwenyezi-Mungu alipoona kwamba Lea anachukiwa, akamjalia watoto; lakini Raheli alikuwa tasa. Lea akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Reubeni, akisema, “Mwenyezi-Mungu ameyaona mateso yangu; bila shaka sasa mume wangu atanipenda.” Lea akapata mimba tena, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Simeoni, akisema, “Mwenyezi-Mungu amenipa mtoto mwingine wa kiume kwa sababu amesikia jinsi ninavyochukiwa.” Akapata mimba mara nyingine, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Lawi, akisema, “Wakati huu mume wangu atajiunga nami, kwani nimemzalia watoto watatu wa kiume.” Lea akapata mimba tena, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Yuda, akisema, “Safari hii nitamsifu Mwenyezi-Mungu.” Kisha Lea akaacha kuzaa. Raheli alipoona kwamba hajamzalia Yakobo watoto, alimwonea wivu Lea, dada yake, akamwambia Yakobo, “Nipatie watoto, la sivyo, nitakufa.” Yakobo akamkasirikia Raheli sana na kumwambia, “Je, mimi nimekuwa badala ya Mungu aliyekuzuia kupata watoto?” Raheli akamjibu, “Mjakazi wangu Bilha yupo. Lala naye ili azae watoto badala yangu, nami pia nipate watoto kutokana naye.” Kwa hiyo Raheli akampa Yakobo mtumishi wake, Bilha, awe mkewe, naye akalala naye. Bilha akapata mimba na kumzalia Yakobo mtoto wa kiume. Raheli akasema, “Mungu amenitendea sawa, amekisikia kilio changu na kunipa mtoto wa kiume.” Akamwita mtoto huyo Dani. Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena na kumzalia Yakobo mtoto wa pili wa kiume. Hapo Raheli akasema, “Nimepigana miereka mikali na dada yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Naftali. Lea alipoona ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, na kumpa Yakobo ili awe mkewe. Zilpa akamzalia Yakobo mtoto wa kiume. Lea akasema, “Bahati njema.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Gadi. Zilpa, mtumishi wa Lea, alimzalia Yakobo mtoto wa pili wa kiume. Lea akasema, “Bahati njema! Sasa wanawake wataniita heri.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Asheri. Ikawa wakati wa mavuno ya ngano, Reubeni alikwenda shambani na huko akapata tunguja, akamletea mama yake Lea. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali, nipe baadhi ya tunguja za mwanao.” Lakini Lea akamsemea kwa ukali, “Je, unadhani ni jambo dogo kuninyanganya mume wangu, na sasa unataka kuchukua tunguja za mwanangu?” Raheli akamjibu, “Ikiwa utanipa tunguja za mwanao, Yakobo atalala kwako leo.” Basi, jioni Yakobo alipokuwa anarudi toka shambani, Lea alitoka kwenda kumlaki, akamwambia, “Leo huna budi kulala nami, kwani nimekuajiri kwa tunguja za mwanangu.” Hivyo Yakobo akalala kwa Lea usiku huo. Mungu akasikiliza ombi la Lea, naye akapata mimba na kumzalia Yakobo mtoto wa tano wa kiume. Lea akasema, “Mungu amenipa ujira wangu kwa sababu nilimpa mume wangu mjakazi wangu.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Isakari. Lea akapata mimba tena na kumzalia Yakobo mtoto wa sita wa kiume. Akasema, “Mungu amenipa zawadi bora. Sasa mume wangu ataniheshimu kwa maana nimemzalia watoto sita wa kiume.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Zebuluni. Baadaye akazaa mtoto wa kike, akamwita Dina. Kisha Mungu akamkumbuka Raheli, akalikubali ombi lake na kumjalia kupata watoto. Raheli akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume, akasema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Yosefu akisema, “Mwenyezi-Mungu na aniongezee mtoto mwingine wa kiume.” Baada ya Raheli kumzaa Yosefu, Yakobo akamwambia Labani, “Niruhusu nirudi nyumbani, katika nchi yangu. Nipe wake zangu na watoto wangu ambao nimejipatia kutokana na utumishi wangu kwako, niondoke nao. Unajua kwamba nimekutumikia vema.” Lakini Labani akamwambia, “Hebu niruhusu nami niseme. Nimetambua kwa kuagua kwamba Mwenyezi-Mungu amenibariki kwa sababu yako. Taja ujira wako, nami nitakulipa.” Yakobo akamwambia, “Wewe mwenyewe unajua jinsi nilivyokutumikia, na jinsi nilivyowatunza wanyama wako. Kwa kuwa kabla sijaja ulikuwa na mali chache tu lakini tangu nifike, mali yako imeongezeka kwa wingi sana, na Mwenyezi-Mungu amekubariki kila nilikokwenda. Lakini sasa, nitaitunza lini jamaa yangu mwenyewe?” Labani akamwuliza, “Nikupatie nini?” Yakobo akamjibu, “Hutanipatia chochote. Nitaendelea kuwatunza wanyama wako ikiwa utanifanyia jambo hili: Niruhusu nipite kati ya wanyama wako wote leo, nitenge katika kundi kila kondoo mwenye madoadoa na mabakamabaka, kila kondoo mweusi, na mbuzi walio na madoadoa na mabakamabaka. Huo ndio utakaokuwa ujira wangu. Hivyo, siku zijazo, uaminifu wangu utaonekana waziwazi utakapokuja kuuangalia ujira wangu. Mbuzi yeyote asiye na madoadoa au mabakamabaka, au kondoo yeyote asiye mweusi akionekana katika kundi langu, huyo atakuwa ameibiwa.” Labani akasema, “Vema! Na iwe kama ulivyosema.” Lakini siku hiyohiyo Labani akaenda akawatenga mabeberu wote wenye milia na madoadoa, mbuzi wote majike waliokuwa na madoadoa na mabakamabaka, kila mnyama aliyekuwa na weupe mwilini mwake, na kila kondoo mweusi, akawaweka chini ya ulinzi wa wanawe. Labani akajitenga na Yakobo umbali wa mwendo wa siku tatu; naye Yakobo akabaki akichunga wanyama wa Labani waliosalia. Basi, Yakobo akatwaa fito mbichi za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni, akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo. Akazisimamisha fito hizo alizozibambua mbele ya wanyama katika mabirika ya kunyweshea maji, mahali ambapo wanyama walikuja kunywa maji. Na kwa kuwa wanyama walichukua mimba walipokuja kunywa maji, wakapata mimba mbele ya hizo fito; wakazaa wanyama wenye milia, mabakamabaka na madoadoa. Yakobo akawatenga hao wanakondoo, kisha akawaelekeza kwenye wanyama wenye milia na weusi katika kundi la Labani. Kwa njia hii, Yakobo akajipatia kundi lake mwenyewe, wala hakulichanganya na lile la Labani. Ikawa kila yalipofika majira ya wanyama wenye afya kuchukua mimba, Yakobo aliziweka zile fito mbele yao katika mabirika ya kunyweshea maji, ili wachukue mimba penye fito hizo. Lakini hakuziweka fito hizo mbele ya wanyama dhaifu walipochukua mimba. Punde si punde, wanyama dhaifu wakawa wa Labani, na wenye afya wakawa wa Yakobo. Basi, Yakobo akatajirika sana, akawa na makundi makubwa ya wanyama, watumishi wa kike na wa kiume, ngamia na punda. Basi, ikasikika kwamba watoto wa kiume wa Labani walinungunika na kusema, “Yakobo amenyakua kila kitu cha baba yetu; ndivyo alivyopata kuwa tajiri.” Yakobo alijua pia kuwa Labani hakumjali yeye kama hapo awali. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya wazee wako na kwa jamaa yako, nami nitakuwa pamoja nawe.” Basi Yakobo akataka Raheli na Lea waitwe; nao wakamwendea mbugani alikokuwa anachunga wanyama. Yakobo akawaambia, “Naona kuwa baba yenu hanijali tena kama hapo awali. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote. Hata hivyo yeye amenidanganya na kuubadilisha ujira wangu mara kumi. Lakini Mungu hakumruhusu kunidhuru. Kila mara baba yenu aliposema, ‘Wanyama wenye madoadoa ndio watakaokuwa ujira wako,’ basi kundi lote lilizaa wanyama wenye madoadoa. Na kila aliposema, ‘Wanyama wenye milia ndio watakaokuwa ujira wako,’ basi, kundi lote lilizaa wanyama wenye milia. Ndivyo Mungu alivyochukua wanyama wa baba yenu, akanipa mimi. “Wakati wa majira ya wanyama kupata mimba niliota ndoto, na katika ndoto hiyo niliona mabeberu wote waliopanda majike walikuwa wenye milia, madoadoa na mabakamabaka. Malaika wa Mungu akaongea nami katika ndoto hiyo, akaniita, ‘Yakobo,’ nami nikaitika, ‘Naam!’ Naye akaniambia, ‘Tazama mabeberu wote wanaowapanda majike wana milia, madoadoa na mabaka mabaka. Jambo hili limekuwa hivyo kwa sababu nimeona alivyokutendea Labani. Mimi ndimi yule Mungu aliyekutokea kule Betheli, mahali pale ulipoweka lile jiwe wakfu kwa kulimiminia mafuta na ambapo uliniwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii urudi katika nchi yako.’” Raheli na Lea wakamjibu Yakobo, “Sisi hatuna tena sehemu au urithi wowote katika nyumba ya baba yetu! Aidha yeye anatuona sisi kama wageni, kwa maana ametuuza; na mali ileile tuliyonunuliwa nayo ndiyo anayotumia. Mali yote ambayo Mungu ameichukua kutoka kwa baba yetu ni yetu sisi na watoto wetu. Kwa hiyo, fanya hayo aliyokuagiza Mungu!” Basi, Yakobo akajitayarisha kusafiri, akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia. Alichukua wanyama wake wote pamoja na mali yote aliyochuma huko Padan-aramu, akaanza safari ya kurudi nchini Kanaani kwa baba yake Isaka. Wakati huo Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya wanyama wake. Hivyo Raheli alipata nafasi ya kuiba vinyago vya miungu ya baba yake. Yakobo alimdanganya Labani, Mwaramu, kwa kuondoka bila kumjulisha. Basi, Yakobo akachukua mali yake yote, akatoroka. Baada ya kuvuka mto Eufrate, alielekea Gileadi, nchi ya milima. Siku tatu baadaye, Labani alijulishwa kwamba Yakobo amemtoroka. Basi, Labani akawachukua ndugu zake, akamfuata Yakobo kwa muda wa siku saba, akamkuta milimani, nchini Gileadi. Lakini usiku, Mungu akamtokea Labani, Mwaramu, katika ndoto, akamwambia, “Jihadhari! Usimwambie Yakobo neno lolote lile, jema au baya.” Basi, Labani akamfikia Yakobo. Wakati huo Yakobo alikuwa amepiga kambi yake milimani. Labani naye, pamoja na ndugu zake, akapiga kambi yake kwenye milima ya Gileadi. Ndipo Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini? Mbona umenidanganya, ukawachukua binti zangu kama mateka vitani? Kwa nini ulitoroka kisiri, ukanihadaa, wala hukuniarifu ili nipate kukuaga kwa shangwe, nyimbo, matari na vinubi? Mbona hukunipa fursa ya kuwabusu kwaheri binti zangu na wajukuu zangu? Kweli umetenda kipumbavu! Nina uwezo wa kukudhuru; lakini Mungu wa baba yako alinitokea usiku wa kuamkia leo, akanitahadharisha akisema, ‘Jihadhari! Usimwambie Yakobo neno lolote lile, jema au baya’. Najua ulitoroka kwa sababu ya hamu kubwa ya kurudi nyumbani kwa baba yako. Lakini kwa nini uliiba vinyago vya miungu yangu?” Yakobo akamjibu, “Niliogopa kwa sababu nilidhani ungelininyanganya binti zako. Lakini utakayempata na vinyago vya miungu yako asiishi! Mbele ya hawa ndugu zetu, onesha chochote kilicho chako, ukichukue.” Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiba vinyago vya miungu ya Labani. Basi, Labani akatafuta vinyago hivyo vya miungu yake katika hema la Yakobo, la Lea na la wale wajakazi wawili; lakini hakuvipata. Akatoka katika hema la Lea na kuingia hema la Raheli. Raheli alikuwa amevichukua hivyo vinyago, akavificha chini ya matandiko ya ngamia na kuketi juu yake. Labani akavitafuta katika hema lote; lakini hakuvipata. Ndipo Raheli akamwambia baba yake, “Samahani baba, usiudhike, kwani siwezi kusimama mbele yako kwa sababu nimo katika siku zangu.” Basi, Labani akavitafuta vinyago vya miungu yake, lakini hakuvipata. Ndipo Yakobo akakasirika, akamshutumu Labani akisema, “Kosa langu ni nini? Je, umepata nini kilicho chako hata baada ya kuipekua mizigo yangu yote? Kiweke mbele ya ndugu zangu na ndugu zako, ili wao waamue kati yetu sisi wawili! Nimekaa nawe kwa muda wa miaka ishirini; na muda huo wote kondoo wako, wala mbuzi wako hawajapata kuharibu mimba, wala sijawahi kula kondoo dume wa kundi lako. Mimi sikukuletea hata mara moja mnyama wako aliyeuawa na mnyama wa porini, bali nilifidia hasara hiyo mimi mwenyewe. Wewe ulinitaka nilipe bila kujali kama aliibiwa mchana au usiku! Hivyo, mchana nilistahimili jua kali na usiku baridi ilinipiga hata nisiweze kupata usingizi hata kidogo. Kwa miaka ishirini hii yote nimeishi nyumbani kwako. Nilikutumikia miaka kumi na minne kwa ajili ya binti zako wawili, na miaka sita nikawachunga wanyama wako. Lakini wewe, ukabadilisha ujira wangu mara kumi. Kama Mungu wa babu yangu Abrahamu, Mungu ambaye alimfanya baba yangu Isaka kutetemeka, asingelikuwa upande wangu, hakika ungeliniacha niondoke mikono mitupu. Lakini Mungu aliyaona mateso yangu na kazi niliyofanya kwa mikono yangu, akakukemea usiku wa kuamkia leo.” Hapo Labani akamjibu Yakobo, “Binti hawa ni binti zangu, watoto hawa ni watoto wangu, wanyama hawa ni wanyama wangu, na yote unayoyaona hapa ni yangu. Lakini mimi ninaweza kufanya nini leo juu ya hawa binti zangu na watoto wao waliowazaa? Basi, tufanye agano mimi nawe, liwe ushahidi kati yako nami.” Basi, Yakobo akachukua jiwe, akalisimika kama nguzo ya ukumbusho. Tena Yakobo akawaambia ndugu zake, “Kusanyeni mawe.” Nao wakakusanya mawe na kufanya rundo. Kisha wakala chakula karibu na rundo hilo la mawe. Labani akaliita rundo hilo Yegar-sahadutha, lakini Yakobo akaliita Galeedi. Labani akasema, “Rundo hili ni ushahidi kati yako na mimi leo.” Kwa hiyo Labani akaliita Galeedi, na ile nguzo akaiita Mizpa akisema, “Mwenyezi-Mungu na atulinde tuwapo mbali bila kuonana. Kama ukiwatesa binti zangu, au ukioa wanawake wengine zaidi ya hawa, basi ujue kwamba hakuna aliye shahidi kati yetu ila Mungu mwenyewe.” Halafu Labani akamwambia Yakobo, “Tazama rundo hili la mawe na nguzo ambayo nimeisimika kati yako nami. Rundo hili ni ushahidi na nguzo hii ni ushahidi kwamba mimi sitavuka rundo hili kuja kwako kukudhuru, na wala wewe hutavuka rundo hili na nguzo hii kuja kwangu kunidhuru. Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Nahori, ataamua kati yetu.” Basi, Yakobo akaapa kwa Mungu ambaye alimfanya baba yake Isaka, kutetemeka. Kisha akatoa tambiko huko mlimani na kuwaalika ndugu zake wale chakula. Baada ya kula, wakabaki huko usiku kucha. Asubuhi na mapema Labani akaamka, akawabusu wajukuu na binti zake, akawabariki. Kisha akaondoka, akarudi nyumbani. Yakobo aliendelea na safari yake. Basi, malaika wa Mungu wakakutana naye. Yakobo alipowaona, akasema, “Hili ni jeshi la Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali hapo Mahanaimu. Yakobo aliwatuma wajumbe wamtangulie kwenda kwa nduguye Esau, huko Seiri, katika nchi ya Edomu. Aliwapa maagizo haya, “Mtamwambia bwana wangu Esau hivi: Mtumishi wako Yakobo asema hivi, ‘Nimekaa ugenini kwa Labani mpaka sasa. Nina ng'ombe, punda, makundi ya kondoo na watumishi wa kiume na wa kike. Ninakutumia ujumbe huu, bwana wangu, ili nipate fadhili mbele yako.’” Hao wajumbe walikwenda, kisha wakarudi na kumwambia Yakobo, “Tumefika kwa ndugu yako Esau, naye yuko njiani kuja kukulaki, akiwa na watu 400.” Basi, Yakobo akaogopa sana na kufadhaika. Akawagawa katika makundi mawili watu waliokuwa pamoja naye, kondoo, mifugo mingine na ngamia, akifikiri, “Kama Esau akija na kuliangamiza kundi moja, basi, kundi litakalosalia litaponyoka.” Kisha Yakobo akamwomba Mungu akisema, “Ee Mungu wa babu yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaka! Ewe Mwenyezi-Mungu uliyeniambia nirudi katika nchi yangu kwa jamaa yangu, ukaniahidi kunitendea mema, sistahili hata kidogo fadhili ulizonipa kwa uaminifu mimi mtumishi wako. Nilipovuka mto Yordani, sikuwa na kitu ila fimbo; lakini sasa ninayo makundi haya mawili. Nakuomba uniokoe sasa kutoka kwa ndugu yangu Esau, maana nina hofu kuwa atatushambulia na kutuua sote, akina mama pamoja na watoto. Wewe uliniahidi kunitendea mema na kuwafanya wazawa wangu wawe wengi kama mchanga wa bahari ambao hauhesabiki kwa wingi wake.” Basi, Yakobo akalala hapo usiku huo. Kisha akatenga sehemu ya mali yake, iwe zawadi kwa ndugu yake Esau: Mbuzi majike 200 na mabeberu 20, kondoo majike 200 na madume 20, ngamia 30 wanyonyeshao pamoja na ndama wao, ng'ombe majike 40 na mafahali kumi, na punda majike 20 na madume kumi. Akawakabidhi watumishi wake, kila mmoja kundi lake, akawaambia, “Nitangulieni mkiacha nafasi kati ya kundi na kundi katika msafara wenu.” Akamwagiza yule aliyetangulia, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni mtumishi wa nani? Unakwenda wapi? Na wanyama hawa ni wa nani?’ Wewe utamjibu, ‘Hii ni mali ya mtumishi wako Yakobo, nayo ni zawadi yako wewe bwana wangu Esau. Tena Yakobo mwenyewe yuko nyuma anafuata.’” Akatoa agizo hilohilo kwa mtumishi wa kundi la pili na la tatu na wengine wote, akisema, “Mtamwambia Esau maneno hayohayo mtakapokutana naye. Zaidi ya yote, mtamwambia, ‘Mtumishi wako Yakobo yuko nyuma, anafuata.’” Yakobo alifanya hivyo akifikiri, “Pengine nitamtuliza kwa zawadi hizi ninazomtangulizia, na baadaye naweza kuonana naye ana kwa ana; huenda atanipokea.” Basi, akatanguliza zawadi zake, lakini yeye mwenyewe akalala kambini usiku huo. Usiku huohuo Yakobo akaamka, akawachukua wake zake wawili, wajakazi wake wawili na watoto wake kumi na mmoja, akapita kivuko cha Yaboki. Baada ya kuwavusha ngambo ya kijito wale waliokuwa nao na mali yake yote, Yakobo alibaki peke yake. Mtu mmoja akaja, akapigana naye mwereka mpaka alfajiri. Mtu huyo alipoona kwamba hawezi kumshinda Yakobo, alimgusa Yakobo nyonga ya kiuno, naye akateguka alipokuwa anapigana naye mwereka. Kisha yule mtu akamwambia Yakobo, “Niache niende zangu, kwani kunapambazuka.” Lakini Yakobo akamwambia, “Sikuachi kamwe, mpaka umenibariki!” Naye akamwuliza, “Jina lako nani?” Yeye akamjibu, “Yakobo.” Yule mtu akamwambia, “Hutaitwa Yakobo tena, bali Israeli, kwa kuwa umeshindana na Mungu na wanadamu, ukashinda.” Ndipo Yakobo akamwambia, “Tafadhali, nakuomba uniambie jina lako.” Lakini yeye akamwambia, “Ya nini kuniuliza jina langu?” Kisha akambariki Yakobo. Yakobo akapaita mahali hapo Penueli, akisema, “Nimemwona Mungu uso kwa uso, nami sikufa.” Jua lilikuwa limekwisha chomoza wakati Yakobo alipoondoka Penueli; akawa anachechemea kwa sababu ya kiuno chake. Ndiyo maana mpaka leo Waisraeli hawali msuli wa nyonga, kwa maana yule mtu alimgusa Yakobo panapo nyonga katika msuli wa kiuno chake. Basi, Yakobo alitazama, akamwona Esau akija pamoja na watu 400. Hapo, akawagawa watoto wake kati ya Lea, Raheli na wale wajakazi wawili. Akawaweka wajakazi na watoto wao mbele, kisha Lea na watoto wake, na nyuma kabisa wakafuata Raheli na mwanawe Yosefu. Kisha yeye mwenyewe akawatangulia, akaenda akiinama mpaka chini kwa heshima mara saba, mpaka alipofika karibu na ndugu yake. Basi, Esau akaenda mbio kumlaki Yakobo, akamkumbatia na kumbusu shingoni, na wote wawili wakalia. Esau alipotazama na kuwaona wale kina mama na watoto, akauliza, “Ni kina nani hawa ulio nao?” Yakobo akamjibu, “Hawa ni watoto ambao Mungu, kwa neema yake, amenijalia mimi mtumishi wako.” Kisha wale wajakazi wakakaribia pamoja na watoto wao, wakainama kwa heshima. Hali kadhalika Lea akaja pamoja na watoto wake, akainama kwa heshima. Hatimaye, Raheli na Yosefu wakaja, wakainama kwa heshima. Ndipo Esau akauliza, “Nini maana ya kundi hili nililokutana nalo njiani?” Yakobo akamjibu, “Nilitumaini kupata fadhili kwako ee bwana wangu.” Lakini Esau akasema, “Nina mali ya kutosha ndugu yangu. Mali yako na iwe yako mwenyewe.” Yakobo akamwambia, “La! Kama kweli umekubali kunipokea, basi, nakusihi uipokee zawadi yangu. Hakika, kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa vile ulivyonipokea kwa wema mkubwa. Basi, nakuomba uikubali zawadi niliyokuletea, kwa sababu hata mimi pia Mungu amenineemesha, nami ninayo mali nyingi.” Ndivyo Yakobo alivyomshawishi Esau, naye akaipokea zawadi yake. Esau akasema, “Haya! Tuendelee na safari yetu; mimi nitakutangulia.” Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu, wewe unajua kwamba watoto hawa ni wachanga, na kwamba mifugo hii inanyonyesha, nami sina budi kuitunza; kama wanyama hawa watapelekwa mbio kwa siku moja, wote watakufa. Basi, nakuomba utangulie, nami nitafuata polepole kadiri ya mwendo wa wanyama na watoto, mpaka nitakapokufikia huko Seiri.” Hapo Esau akasema, “Heri nikuachie baadhi ya watu wangu.” Lakini Yakobo akasema, “Kuna haja gani ya kufanya hivyo? Yanitosha kwamba mimi nimepata fadhili yako, ewe bwana wangu.” Basi, siku hiyo Esau akaanza safari ya kurudi Seiri. Lakini Yakobo akasafiri kwenda Sukothi, na huko akajijengea nyumba na vibanda kwa ajili ya wanyama wake. Kwa sababu hiyo, mahali hapo pakaitwa Sukothi. Kutoka Padan-aramu, Yakobo alifika salama mjini Shekemu, katika nchi ya Kanaani, akapiga kambi yake karibu na mji huo. Sehemu hiyo ya ardhi ambako alipiga kambi aliinunua kutoka kwa wazawa wa Hamori, baba yake Shekemu, kwa vipande 100 vya fedha. Huko, akajenga madhabahu na kupaita Mungu ni Mungu wa Israeli. Siku moja, Dina, binti yake Yakobo na Lea, alikwenda kuwatembelea wanawake wa nchi hiyo. Basi, Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, aliyekuwa mkuu wa nchi hiyo, alipomwona Dina, akamshika, akalala naye kwa nguvu. Lakini Shekemu akavutiwa sana na huyo msichana, akampenda hata akaanza kumbembeleza. Kwa hiyo, Shekemu akazungumza na Hamori baba yake, akamwambia, “Tafadhali, niombee huyo msichana nimwoe.” Yakobo akapata habari kwamba Dina, bintiye, alikuwa amenajisiwa na Shekemu; lakini kwa kuwa wanawe walikuwa malishoni, alinyamaza mpaka waliporudi. Hamori, baba yake Shekemu, akaenda kwa Yakobo ili azungumze naye, na wakati huohuo watoto wa kiume wa Yakobo wakawa wanarudi nyumbani kutoka malishoni. Waliposikia hayo, vijana hao wakaona uchungu mwingi na kukasirika sana, kwa vile Shekemu alikuwa amewafanyia watu wa Israeli ovu hilo la kulala na binti ya Yakobo, maana jambo hilo lilikuwa mwiko. Lakini Hamori akawaambia, “Mwanangu Shekemu anampenda sana binti yenu. Basi, tafadhali mumruhusu amwoe. Acheni tuoane: Nyinyi mtatuoza binti zenu, nasi tutawaoza binti zetu. Kwa hiyo mtaishi pamoja nasi; mtakuwa huru katika nchi hii. Mtaishi humu, mfanye biashara na kujipatia mali.” Hali kadhalika, Shekemu akawaambia baba na ndugu zake Dina, “Tafadhali, mniwie radhi, nami nitawapeni chochote mtakachosema. Niambieni kiasi chochote cha mahari na zawadi, hata kikiwa kikubwa namna gani, nami nitatoa, mradi tu mnioze msichana huyu.” Basi, watoto wa kiume wa Yakobo wakamjibu Shekemu na baba yake Hamori kwa hila, kwa kuwa Shekemu alikuwa amekwisha mnajisi dada yao Dina. Waliwaambia, “Hatuwezi kumwoza dada yetu kwa mtu asiyetahiriwa. Kufanya hivyo ni aibu kwetu. Tutakubaliana nanyi tu kwa sharti hili: Kwamba mtakuwa kama sisi kwa kumtahiri kila mwanamume miongoni mwenu. Hapo ndipo tutakapowaoza binti zetu na kuwaoa binti zenu; tutaishi pamoja nanyi na kuwa jamaa moja. Lakini msipokubaliana nasi na kutahiriwa, basi, sisi tutamchukua binti yetu na kwenda zetu.” Pendekezo lao likawapendeza Hamori na mwanawe Shekemu. Kijana huyo hakusita hata kidogo kutekeleza sharti hilo, kwa vile alivyompenda binti wa Yakobo. Isitoshe, Shekemu ndiye aliyeheshimika kuliko wote nyumbani kwao. Basi, Hamori na mwanawe, Shekemu, wakaenda kwenye lango la mji, mahali pa mikutano, wakaongea na watu wao wakisema, “Watu hawa ni marafiki zetu. Tuwakaribishe waishi nchini mwetu na kufanya biashara, kwa sababu tunayo nchi ya kututosha sisi na wao pia; kisha tutaoa binti zao na kuwaoza binti zetu. Lakini wao watakubali kuishi nasi na tutakuwa jamaa moja kwa sharti hili: Kwamba tutamtahiri kila mwanamume miongoni mwetu kama wao walivyotahiriwa. Je, hamwoni kwamba mifugo yao na mali yao yote itakuwa mali yetu? Haya, tukubaliane nao ili wakae pamoja nasi.” Wanaume wote waliokusanyika penye lango la mji huo wakakubaliana na Hamori na mwanawe Shekemu. Kisha, wanaume wote wakatahiriwa. Siku tatu baadaye, waliotahiriwa wakiwa bado wana maumivu makali, watoto wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, kaka zake Dina, walizitwaa panga zao, wakauvamia mji ghafla na kuwaua wanaume wote. Waliwaua kwa upanga Hamori na mwanawe Shekemu, wakamtoa Dina katika nyumba ya Shekemu, wakaenda zao. Baada ya mauaji hayo, watoto wengine wa kiume wa Yakobo waliingia mjini na kuuteka nyara mji huo, kwa sababu dada yao alikuwa amenajisiwa. Walichukua kondoo na mbuzi, ng'ombe, punda na chochote kilichokuwa mjini au shambani. Waliteka nyara mali yote, watoto na wanawake wote na chochote kilichokuwa majumbani. Basi, Yakobo akamwambia Simeoni na Lawi, “Nyinyi mmeniletea taabu kwa kunifanya nichukiwe na wakazi wa nchi hii ya Wakanaani na Waperizi. Mimi sina watu wengi, na kama wakikusanyika kunishambulia wataniangamiza mimi pamoja na jamaa yangu.” Hao ndugu wawili wakajibu, “Ana haki gani ya kumtendea dada yetu kama malaya?” Siku moja, Mungu alimwambia Yakobo, “Anza safari, uende kuishi Betheli na kunijengea humo mahali pa kunitambikia mimi Mungu niliyekutokea wakati ulipomkimbia kaka yako Esau.” Basi, Yakobo akawaambia jamaa yake na wote aliokuwa nao, “Tupilieni mbali sanamu za miungu ya kigeni mlizo nazo, mjitakase na kubadili mavazi yenu. Kisha, tutakwenda Betheli ili nimjengee mahali pa kumtambikia Mungu aliyenisaidia siku ya taabu, Mungu ambaye amekuwa nami popote nilipokwenda.” Basi, wakampa Yakobo sanamu zote za miungu ya kigeni walizokuwa nazo pamoja na vipuli walivyokuwa wamevaa masikioni; naye akavifukia chini ya mwaloni uliokuwa karibu na Shekemu. Yakobo na wanawe walipokuwa wanasafiri, Mungu aliwatia hofu wenyeji wa miji yote ya jirani hata hawakuthubutu kuwafuatia. Basi, Yakobo akawasili Luzu yaani Betheli katika nchi ya Kanaani, pamoja na watu wote aliokuwa nao. Akajenga hapo madhabahu na kupaita El-betheli kwani hapo ndipo mahali Mungu alipojionesha kwake wakati alipokuwa akimkimbia kaka yake. Debora, mlezi wa Rebeka, alifariki, akazikwa chini ya mwaloni upande wa kusini wa Betheli. Kwa hiyo Yakobo akauita mji huo Alon-bakuthi. Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki. Mungu alimwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa hivyo tena, bali sasa jina lako litakuwa Israeli.” Kwa hiyo Yakobo akaitwa Israeli. Tena Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu mwenye nguvu. Ujaliwe wazawa wengi; kwako wewe kutatokea taifa, mataifa na wafalme. Nchi niliyowapa Abrahamu na Isaka, nitakupa wewe na wazawa wako.” Basi, baada ya kuongea na Yakobo, Mungu akamwacha na kupanda juu. Yakobo akasimika nguzo ya jiwe la ukumbusho mahali hapo Mungu alipozungumza naye, akaiweka wakfu kwa kuimiminia tambiko ya kinywaji na mafuta. Basi, Yakobo akapaita mahali hapo alipozungumza na Mungu Betheli. Yakobo na jamaa yake yote waliendelea na safari yao kutoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efratha, Raheli akashikwa na uchungu mkali wa kuzaa. Naye alipokuwa katika uchungu huo, mkunga akamwambia, “Usiogope, umepata mtoto mwingine wa kiume.” Raheli huku akikata roho, akampa huyo mtoto jina Ben-oni. Lakini baba yake akamwita mtoto huyo Benyamini. Basi, Raheli akafariki na kuzikwa kando ya njia iendayo Efratha (yaani Bethlehemu). Yakobo akasimika nguzo ya kumbukumbu juu ya kaburi la Raheli ambayo ipo mpaka leo. Israeli akaendelea na safari yake na kupiga kambi yake baada ya kuupita mnara wa Ederi. Wakati Israeli alipokuwa anakaa nchini humo, mwanawe Reubeni, alilala na Bilha, suria wa baba yake; naye Israeli akasikia habari hizo. Yakobo alikuwa na watoto wa kiume kumi na wawili. Wana wa Lea walikuwa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zebuluni. Watoto wa kiume wa Raheli walikuwa Yosefu na Benyamini. Watoto wa kiume waliozaliwa na Bilha, mjakazi wa Raheli, walikuwa Dani na Naftali. Na watoto wa kiume waliozaliwa na Zilpa, mjakazi wa Lea, walikuwa Gadi na Asheri. Hao ndio watoto wa kiume wa Yakobo, aliowazaa alipokuwa kule Padan-aramu. Yakobo aliondoka akaenda Mamre kwa baba yake Isaka, huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, mahali ambapo Abrahamu na Isaka walikaa kama wageni. Isaka alikuwa na miaka 180 akafariki akiwa mzee wa miaka mingi. Watoto wake, Esau na Yakobo wakamzika. Wafuatao ni wazawa wa Esau (yaani Edomu). Esau alioa wake Wakanaani: Ada binti Eloni Mhiti, Oholibama binti Ana, binti Sibeoni, Mhivi, na Basemathi, binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi. Ada alimzalia Esau Elifazi, naye Basemathi akamzalia Reueli. Oholibama alimzalia Yeushi, Yalamu na Kora. Hao ndio watoto wa kiume wa Esau ambao wake zake walimzalia alipokaa katika nchi ya Kanaani. Kisha, Esau akawachukua wake zake, watoto wake wa kiume na wa kike, watu wote wa nyumbani mwake, ng'ombe wake, wanyama wake wengine wote na mali yake yote ambayo alikuwa ameipata katika nchi ya Kanaani, akahamia mahali pengine, mbali na nduguye Yakobo. Alifanya hivyo kwa sababu mali zao zilikuwa nyingi hata wasiweze kuishi pamoja. Nchi waliyokaa kama wageni haikuweza kuwatosha kwa sababu ya wingi wa mifugo yao. Kwa hiyo, Esau akaenda kukaa katika nchi ya milima ya Seiri. Jina lingine la Esau ni Edomu. Wafuatao ni wazawa wa Esau, baba ya Waedomu katika nchi ya milima ya Seiri. Watoto wa kiume wa Esau walikuwa Elifazi aliyezaliwa na Ada mkewe, na Reueli aliyezaliwa na Basemathi mke wake mwingine. Watoto wa kiume wa Elifazi walikuwa Temani, Omari, Sefo, Gatamu na Kenazi. Elifazi alikuwa na suria jina lake Timna. Huyu alimzalia mwana, jina lake Amaleki. Basemathi, mkewe Esau, alimzaa Reueli. Watoto wa kiume wa Reueli walikuwa Nahathi, Zera, Shama na Miza. Oholibama, binti Ana, binti Sibeoni, alimzalia Esau mumewe watoto wa kiume watatu: Yeushi, Yalamu na Kora. Wafuatao ni wakuu wa makabila yaliyotokana na Esau. Elifazi, aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Esau aliwazaa Temani, Omari, Sefo, Kenazi, Kora, Gatamu na Amaleki, kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake. Hao wote ni watoto wa kiume wa Elifazi katika nchi ya Edomu, waliotokana na Ada, mkewe Esau. Reueli, mwanawe Esau, aliwazaa Nahathi, Zera, Shama na Miza, kila mmoja wao akawa mkuu wa kabila lake. Hao wote ni watoto wa kiume wa Reueli katika nchi ya Edomu, waliotokana na Basemathi, mkewe Esau. Watoto wa kiume wa Oholibama, mkewe Esau, walikuwa Yeushi, Yalamu na Kora, kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake. Hao wote ni watoto wa kiume wa Oholibama, binti Ana, mkewe Esau. Basi, hao ndio wazawa wa Esau yaani Edomu, kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake. Wafuatao ni wazawa wa Seiri, Mhori, na ndio wenyeji wa nchi hiyo: Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana, Dishoni, Eseri na Dishani; kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake miongoni mwa Wahori wa uzawa wa Seiri, katika nchi ya Edomu. Watoto wa kiume wa Lotani walikuwa Hori na Hemani; na dada yake Lotani aliitwa Timna. Watoto wa kiume wa Shobali walikuwa Alvani, Manahathi, Ebali, Shefo na Onamu. Watoto wa kiume wa Sibeoni walikuwa Aya na Ana. Ana ndiye aliyeziona chemchemi za maji ya moto jangwani, alipokuwa anawachunga punda wa baba yake Sibeoni. Watoto wa Ana walikuwa Dishoni na dada yake mmoja aitwaye Oholibama. Watoto wa kiume wa Dishoni walikuwa Hemdani, Eshbani, Ithrani na Kerani. Watoto wa kiume wa Eseri walikuwa Bilhani Zaawani na Akani. Watoto wa kiume wa Dishani walikuwa Usi na Arani. Basi, hao ndio wakuu wa Wahori: Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana, Dishoni, Eseri na Dishani; kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake katika nchi ya Seiri. Wafuatao ni wafalme waliotawala nchi ya Edomu, kabla mfalme yeyote hajawatawala Waisraeli: Bela mwana wa Beori alitawala nchi ya Edomu akiwa na makao yake makuu katika mji wa Dinhaba. Bela alipofariki, Yobabu mwana wa Zera kutoka Bosra alitawala badala yake. Yobabu alipofariki, Hushamu wa nchi ya Watemani, alitawala badala yake. Hushamu alipofariki, Hadadi mwana wa Bedadi alitawala badala yake, makao yake makuu yakiwa katika mji wa Avithi. Huyu ndiye aliyewapiga na kuwashinda Wamidiani katika nchi ya Moabu. Hadadi alipofariki, Samla kutoka Masreka, alitawala badala yake. Samla alipofariki, Shauli kutoka Rehobothi, ulio karibu na mto Eufrate, alitawala badala yake. Shauli alipofariki, Baal-hanani, mwana wa Akbori, alitawala badala yake. Baal-hanani, mwana wa Akbori alipofariki, Hadadi alitawala badala yake, na jina la mji wake likiwa Pau. Mkewe Akbori alikuwa Mehetabeli, binti Matredi na mjukuu wa Mezahabu. Wakuu wa makabila yaliyotokana na Esau, kadiri ya makabila yao na makazi yao walikuwa: Timna, Alva, Yethethi, Oholibama, Ela, Pinoni, Kenazi, Temani, Mibsari, Magdieli na Iramu. Hao ndio wakuu wa makabila yaliyotokana na Edomu, yaani Esau, baba yake Edomu; wametajwa kulingana na makazi yao katika sehemu za nchi walizomiliki. Yakobo aliendelea kukaa katika nchi ya Kanaani, alimoishi baba yake kama mgeni. Hizi ndizo habari za ukoo wa Yakobo. Yosefu, akiwa kijana wa umri wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake, wana wa Bilha na Zilpa, wake za baba yake. Yosefu akawa anamjulisha baba yake juu ya tabia mbaya za ndugu zake. Israeli alimpenda Yosefu kuliko watoto wake wote kwa sababu alikuwa amezaliwa wakati wa uzee wake. Alimshonea Yosefu kanzu ndefu. Lakini ndugu zake walipoona kwamba baba yao alimpenda Yosefu kuliko wao, wakamchukia hata hawakuzungumza naye kwa amani. Usiku mmoja, Yosefu aliota ndoto, lakini alipowasimulia ndugu zake, wao wakazidi kumchukia. Aliwaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota: Niliota kuwa sote tulikuwa shambani tukifunga miganda na ghafla mganda wangu ukainuka na kusimama wima. Miganda yenu ikakusanyika kuuzunguka na kuuinamia mganda wangu.” Ndugu zake wakamwuliza, “Je, unataka kutuambia kwamba utatutawala? Au utakuwa na mamlaka juu yetu?” Basi, wakazidi kumchukia kwa sababu ya ndoto na maneno yake. Kisha Yosefu akaota ndoto nyingine, akawasimulia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine; nimeona jua, mwezi na nyota kumi na moja vinaniinamia.” Lakini alipomsimulia baba yake na ndugu zake ndoto hiyo, baba yake alimkemea akisema, “Ni ndoto gani hiyo uliyoota? Je, itatulazimu mimi, mama yako na ndugu zako kuja kuinama chini kwa heshima mbele yako?” Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akawa analifikiria jambo hilo. Siku moja, ndugu zake Yosefu walikwenda kuchunga wanyama wa baba yao karibu na Shekemu. Basi, Israeli akamwambia Yosefu, “Unajua ndugu zako wanachunga wanyama kule Shekemu. Kwa hiyo nataka nikutume kwao.” Yosefu akajibu, “Niko tayari.” Baba yake akamwambia, “Nenda ukawaangalie ndugu zako na wanyama kama wako salama, kisha uniletee habari.” Basi, Yakobo akamtuma Yosefu kutoka bonde la Hebroni. Yosefu alipokaribia Shekemu mtu mmoja akamkuta akitangatanga mbugani, akamwuliza, “Unatafuta nini?” Yosefu akamjibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Tafadhali, niambie mahali wanakochunga wanyama.” Yule mtu akamwambia, “Bila shaka wamekwisha ondoka, kwa sababu niliwasikia wakisema kwamba wanakwenda Dothani.” Basi, Yosefu akawafuata ndugu zake, akawakuta huko Dothani. Ndugu zake walipomwona akiwa mbali na kabla hajafika karibu, wakafanya mpango wa kumuua. Waliambiana, “Tazameni! Yule mwota ndoto anakuja. Haya, tumuue na kumtupa ndani ya shimo mojawapo. Baadaye tutasema kwamba ameuawa na mnyama wa porini. Halafu tutaona hizo ndoto zake zitakuwaje.” Lakini Reubeni aliposikia maneno hayo, akataka kumwokoa mikononi mwao; basi akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, tusimuue. Msimwage damu. Ila mtumbukizeni katika shimo hili hapa mbugani, lakini msimdhuru.” Alisema hivyo kusudi aweze kumwokoa Yosefu mikononi mwao, na baadaye amrudishe kwa baba yake. Yosefu alipowafikia ndugu zake, wao wakamvua kanzu yake. Kisha wakamshika na kumtupa shimoni. Lakini shimo hilo halikuwa na maji. Walipoketi kula, wakaona msafara wa Waishmaeli wakisafiri kutoka Gileadi kwenda Misri. Ngamia wao walikuwa wamebeba ubani, zeri na manemane. Hapo Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutapata faida gani tukimuua ndugu yetu na kuficha mauaji yake? Afadhali tumwuze kwa hawa Waishmaeli, lakini tusiguse maisha yake, kwani yeye ni ndugu yetu; yeye ni damu moja nasi.” Ndugu zake wakakubaliana naye. Wafanyabiashara Wamidiani walipofika mahali hapo, hao ndugu wakamtoa Yosefu katika shimo, wakamwuza kwa Waishmaeli kwa bei ya vipande ishirini vya fedha; nao wakamchukua Yosefu hadi Misri. Basi, Reubeni aliporudi kwenye lile shimo, na asimwone Yosefu tena, akazirarua nguo zake kwa huzuni, akawaendea ndugu zake, akawaambia, “Kijana hayupo nami niende wapi?” Basi, wakachinja mbuzi, wakaichukua kanzu ya Yosefu na kuichovya katika damu ya huyo mbuzi. Kisha wakampelekea baba yao ile kanzu, wakamwambia, “Tumeiokota kanzu hii. Hebu iangalie kama ni ya mwanao, au siyo.” Baba yao akaitambua hiyo kanzu, akasema, “Ndiyo hasa! Bila shaka mnyama wa porini amemshambulia na kumla. Hakika Yosefu ameraruliwa vipandevipande.” Hapo Yakobo akayararua mavazi yake kwa huzuni, akavaa vazi la gunia kiunoni. Akamlilia mwanawe kwa muda wa siku nyingi. Watoto wake wa kiume na wa kike wakamjia ili kumfariji, lakini akakataa kufarijiwa, akisema, “Niacheni; nitaendelea kuomboleza kwa ajili ya mwanangu, mpaka nitakaposhuka kuzimu alipo.” Ndivyo baba yake alivyomlilia. Wakati huo, kule Misri, wale Wamidiani walimwuza Yosefu kwa mtu aitwaye Potifa, mmoja wa maofisa wa Farao, ambaye alikuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi. Wakati huo, Yuda alitengana na ndugu zake, akaenda kukaa na mtu mmoja Mwadulami, jina lake Hira. Akiwa huko, Yuda akamwona binti Shua, Mkanaani, akamwoa. Binti Shua akapata mimba akazaa mtoto wa kiume, Yuda akamwita Eri. Akapata mimba nyingine, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Onani. Kisha akapata mtoto mwingine wa kiume, akamwita Shela. Wakati Shela alipozaliwa, Yuda alikuwa Kezibu. Baadaye Yuda alimwoza mtoto wake wa kwanza Eri, kwa mwanamke aitwaye Tamari. Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; hivyo Mwenyezi-Mungu akamuua. Basi, Yuda akamwambia Onani, “Mchukue mke wa ndugu yako marehemu, kwani ndivyo inavyokupasa kufanya, upate kumzalia nduguyo watoto.” Lakini Onani alijua kwamba hao watoto wasingekuwa wake. Kwa hiyo, alipolala na mke wa nduguye, alimwaga chini mbegu ya uzazi, asije akampatia nduguye watoto. Tendo hilo likamwudhi Mwenyezi-Mungu, akamuua Onani pia. Ndipo Yuda akamwambia Tamari, mke wa mwanawe, “Rudi nyumbani kwa baba yako, ubaki mjane hadi mwanangu Shela atakapokua.” Yuda alihofu Shela naye asije akafa kama ndugu zake. Basi, Tamari akarudi nyumbani kwa baba yake. Kisha binti Shua, mkewe Yuda, akafariki. Yuda alipomaliza kufanya matanga akaondoka na rafiki yake Hira, Mwadulami, wakaenda Timna kwa wakata-manyoya ya kondoo wake. Tamari aliposikia kwamba baba mkwe wake alikuwa njiani kwenda Timna kukata manyoya ya kondoo wake, alivua mavazi yake ya ujane na kujifunika shela kisha akaketi penye lango la kuingilia Enaimu, kijiji kilichokuwa njiani kwenda Timna. Alifanya hivyo kwa vile aliona kwamba Shela alikwisha kuwa mtu mzima, lakini yeye Tamari hakuozwa awe mkewe. Basi, Yuda alipomkuta Tamari hapo, alimdhania kuwa mwanamke malaya, kwani alikuwa amejifunika uso. Hapo, bila kujua kwamba huyo alikuwa mke wa mwanawe, akamwendea pale kando ya njia, akamwambia, “Napenda kulala nawe.” Tamari akamwuliza, “Utanipa nini nikikubali?” Yuda akamjibu, “Nitakupa mwanambuzi kutoka kundi langu.” Tamari akamwambia, “Weka rehani kuthibitisha utaniletea huyo mwanambuzi.” Yuda akamwuliza, “Unataka nikupe nini kama rehani?” Naye akamjibu, “Nipe hiyo pete na kamba yake pamoja na hiyo fimbo unayoshika.” Basi, Yuda akampa vitu hivyo vyote, akalala naye. Tamari akapata mimba yake. Basi, Tamari akarudi nyumbani akavua ile shela aliyojifunika, akavaa tena mavazi yake ya ujane. Wakati Yuda alipomtuma yule rafiki yake, Mwadulami, ampelekee yule mwanamke mwanambuzi ili arudishiwe rehani aliyomwachia, Hira hakumpata. Hira akawauliza wenyeji wa Enaimu, “Yuko wapi yule mwanamke kahaba aliyekuwa kando ya njia karibu na hapa?” Wakamjibu, “Hapa hapajawa na mwanamke kahaba.” Basi, huyo rafiki akarudi kwa Yuda, akamwambia, “Sikumpata! Tena wenyeji wa huko wameniambia kwamba hapajawa na mwanamke kahaba yeyote huko.” Yuda akasema, “Acha avichukue vitu hivyo, la sivyo atatufanya tuchekwe. Wewe mwenyewe umeona kwamba nilimpelekea mwanambuzi, lakini wewe hukumpata.” Baada ya miezi mitatu, Yuda akapata habari, “Tamari, mke wa mwanao amekuwa kahaba, tena amepata mimba kwa kufanya ukahaba.” Basi, Yuda akaamuru, “Mtoeni nje achomwe moto!” Walipokuwa wakimtoa nje, Tamari akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake, akisema, “Mwenye vitu hivi ndiye aliyenipa mimba. Kwa hiyo, nakuomba umtambue mwenye pete hii na kamba yake, na fimbo hii.” Yuda alivitambua vitu hivyo, akasema, “Tamari ni mwadilifu kuliko mimi. Ni kweli, maana sikumwoza kwa mwanangu Shela.” Tokea siku hiyo Yuda hakulala tena na Tamari. Wakati wa kujifungua kwake Tamari ulipofika, ikafahamika kuwa alikuwa na mimba ya mapacha. Basi, alipopata uchungu wa kuzaa pacha mmojawapo alitoa mkono nje, naye mkunga akaufunga kwa uzi mwekundu, akisema, “Huyu ndiye aliyezaliwa kwanza.” Lakini huyo mtoto alipourudisha mkono wake ndani, ndugu yake akazaliwa wa kwanza. Mkunga akasema, “Mbona wewe umepita kwa nguvu?” Kwa hiyo akaitwa Peresi. Baadaye ndugu yake akazaliwa akiwa na ule uzi mwekundu mkononi, naye akaitwa Zera. Basi, Yosefu alipochukuliwa mpaka Misri, Mmisri mmoja aitwaye Potifa ambaye alikuwa ofisa wa Farao na mkuu wa kikosi chake cha ulinzi, akamnunua kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri. Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, akamfanikisha sana. Yosefu akawa anakaa katika nyumba ya bwana wake, Mmisri. Huyo bwana wake akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, na kwamba ndiye aliyeyafanikisha mambo yote aliyofanya Yosefu. Basi, Yosefu akapendeka sana mbele ya Potifa, hata akawa ndiye mtumishi wake binafsi; alimfanya msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake yote. Tokea wakati Potifa alipomfanya Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake, Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya huyo Mmisri kwa ajili ya Yosefu. Baraka za Mwenyezi-Mungu zikawa juu ya kila alichokuwa nacho, nyumbani na shambani. Kwa sababu hiyo Potifa alimpa Yosefu mamlaka juu ya mambo yake yote, naye Potifa akaacha kushughulika na chochote isipokuwa tu chakula chake mwenyewe. Yosefu alikuwa kijana mzuri na wa kupendeza. Basi, baada ya muda fulani, mke wa Potifa akamtamani Yosefu na kumwambia, “Lala na mimi”. Lakini Yosefu akakataa na kumwambia huyo bwana wake, “Kamwe! Bwana wangu amenipa mamlaka juu ya kila kitu hapa nyumbani na, kwa vile niko, hajishughulishi na kitu chochote tena. Hapa nyumbani yeye hana madaraka kuliko mimi. Yeye hakunikataza kushika chochote isipokuwa wewe tu kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu mbaya kama huo, na kumkosea Mungu.” Huyo mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, lakini Yosefu hakumsikiliza wala kukubali kulala naye kamwe. Siku moja, Yosefu aliingia nyumbani kufanya kazi yake kama kawaida, na wafanyakazi wengine hawakuwamo nyumbani. Basi, mke wa Potifa alimshika joho lake na kumwambia, “Lala na mimi!” Lakini Yosefu akamwachia vazi lake mikononi mwake, akakimbilia nje. Hapo, yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu ameliacha vazi lake mikononi mwake na kukimbilia nje, akawaita watumishi wa nyumbani mwake na kuwaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania tuliyeletewa anatuaibisha. Alikuja kwangu akitaka kunishika kwa nguvu, lakini nikapiga kelele. Aliposikia napiga kelele, aliliacha vazi lake, akakimbilia nje!” Basi, yule mwanamke akaliweka vazi hilo mpaka mumewe aliporudi nyumbani. Akamsimulia kisa kile akisema, “Huyu mtumishi Mwebrania uliyemleta kwetu alinijia ili kuniaibisha. Lakini mara tu nilipopiga kelele, aliliacha vazi lake na kukimbilia nje.” Basi, bwana wake Yosefu alipoyasikia maneno ya mkewe, kwamba ndivyo mtumishi wake alivyomtendea, akawaka hasira, akamchukua Yosefu na kumtia gerezani, mahali walipofungwa wahalifu wa mfalme. Lakini hata humo gerezani Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu akimfadhili hata kumfanya apendeke mbele ya mkuu wa gereza. Hivyo mkuu wa gereza alimweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa wote humo gerezani; kila kitu kilichofanyika humo kilifanywa kwa mamlaka yake. Huyo mkuu wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote alichokabidhiwa Yosefu kwa maana Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu na kufanikisha kila kitu alichofanya. Wakati fulani baada ya mambo hayo, maofisa wawili wa mfalme wa Misri walimkosea mfalme. Maofisa hao walikuwa mtunza vinywaji mkuu na mwoka mikate mkuu wa mfalme. Farao aliwakasirikia hao maofisa wake wawili, akawafungia ndani ya ngome ya mkuu wa kikosi cha ulinzi, katika gereza, mahali alipofungwa Yosefu. Mkuu wa kikosi cha ulinzi akamteua Yosefu awatumikie. Nao wakawa kifungoni kwa muda fulani. Basi, usiku mmoja, yule mtunza vinywaji mkuu na yule mwoka mikate mkuu wa mfalme wa Misri, waliota ndoto humo gerezani, kila mmoja na ndoto yake tofauti. Yosefu alipokwenda kwao asubuhi na kuwaona, wote wawili walikuwa wenye wasiwasi. Basi, Yosefu akawauliza maofisa hao wa Farao waliokuwa kifungoni pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, “Mbona leo mna nyuso za huzuni?” Wakamjibu, “Tuna huzuni kwa kuwa tumeota ndoto na hakuna awezaye kututafsiria ndoto zetu.” Yosefu akawaambia, “Je, kutafsiri ndoto si kazi ya Mungu? Basi, niambieni ndoto zenu.” Mtunza vinywaji mkuu wa mfalme akamsimulia Yosefu ndoto yake, akisema, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, nao ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua majani, maua yake yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu mbivu. Mkononi mwangu nilikuwa na kikombe cha Farao, basi, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe hicho, nikampa Farao.” Yosefu akamwambia huyo mtumishi, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Yale matawi matatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani na kukurudisha tena katika cheo chako. Utaweza tena kumpa Farao kikombe mkononi kama ulivyokuwa unafanya hapo awali. Lakini tafadhali usinisahau wakati mambo yatakapokwendea vema; unifanyie fadhili na kunitaja mbele ya Farao, nipate kutoka humu gerezani. Maana mimi nilitoroshwa kutoka nchi ya Waebrania, na hapa Misri sijafanya chochote kinachostahili nitiwe gerezani.” Yule mwoka mikate mkuu alipoona kwamba tafsiri ile ni nzuri, akamwambia Yosefu, “Hata mimi niliota ndoto! Katika ndoto yangu nilikuwa nimechukua kichwani nyungo tatu za mikate. Katika ungo wa juu, kulikuwa na vyakula mbalimbali vilivyookwa kwa ajili ya Farao. Lakini, ndege walikuwa wakivila kutoka ungo huo kichwani pangu!” Yosefu akamwambia, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Zile nyungo tatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani, atakiinua kichwa chako akutundike mtini, nao ndege wataula mwili wako.” Mnamo siku ya tatu, ambayo ilikuwa siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake, Farao aliwaandalia karamu watumishi wake wote. Akawatoa gerezani mtunza vinywaji wake mkuu na mwoka mikate mkuu, akawaweka mbele ya maofisa wake. Kisha akamrudishia cheo chake mtunza vinywaji, apate kumpatia Farao kikombe. Lakini yule mwoka mkate mkuu akamtundika mtini, kama Yosefu alivyokuwa amewatafsiria ndoto zao. Hata hivyo, yule mtunza vinywaji mkuu akamsahau Yosefu, badala ya kumkumbuka. Baada ya miaka miwili mizima, Farao aliota ndoto: Alijikuta amesimama kando ya mto Nili, akaona ng'ombe saba wazuri na wanono wakitoka mtoni na kula nyasi. Halafu, baada ya hao, ng'ombe wengine saba waliokonda sana wakatoka katika mto Nili, wakaja na kusimama karibu na wale ng'ombe wazuri na wanono, kando ya mto. Hao ng'ombe waliokonda sana wakawala wale wengine saba wazuri na wanono. Hapo Farao akaamka usingizini. Alipolala tena, akaota mara ya pili. Aliona masuke saba makubwa na mazuri yanachipuka katika bua moja. Halafu, baada ya hayo, masuke mengine saba membamba na yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani yakatokeza. Hayo masuke saba membamba yakayameza yale masuke saba makubwa yaliyojaa nafaka. Basi, Farao alipoamka akagundua kuwa ilikuwa ndoto. Kulipokuwa asubuhi, Farao akiwa na wasiwasi sana, aliwaita wachawi wote wa Misri, na wenye hekima, akawaambia ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumtafsiria ndoto hizo. Ndipo, yule mtunza vinywaji mkuu akamwambia Farao, “Leo nayakumbuka makosa yangu! Wakati ule ulipotukasirikia sisi watumishi wako, mimi na mwoka mikate mkuu, ulitufungia ndani ya ngome ya mkuu wa kikosi cha ulinzi. Usiku mmoja tuliota ndoto, kila mmoja ndoto yake tofauti. Basi, kijana mmoja Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi, alikuwa pamoja nasi kifungoni. Tulipomsimulia ndoto zetu, yeye aliweza kututafsiria kila mmoja wetu kulingana na ndoto yake. Alivyotafsiri ndivyo ilivyotokea: Mimi nikarudishwa kazini kwangu, na yule mwoka mikate mkuu akatundikwa mtini.” Basi, Farao akaamuru Yosefu aitwe; naye akatolewa gerezani haraka. Baada ya kunyoa na kubadili nguo zake, Yosefu akaja mbele ya Farao. Farao akamwambia Yosefu, “Mimi nimeota ndoto, lakini hakuna mtu aliyeweza kunitafsiria. Nimesikia sifa zako kwamba wewe ukiambiwa ndoto unaweza kuitafsiri.” Yosefu akamjibu Farao, “Sina uwezo huo; lakini Mungu atakupa jibu lifaalo.” Hapo Farao akamwambia Yosefu, “Niliota kwamba nimesimama kando ya mto Nili, nikaona ng'ombe saba wazuri na wanono wakitoka mtoni na kula nyasi. Hao wakafuatwa na ng'ombe wengine saba dhaifu, wembamba na wamekonda sana. Mimi sijapata kamwe kuona ng'ombe wa hali hiyo katika nchi ya Misri. Basi, wale ng'ombe waliokonda sana wakawala wale ng'ombe saba wanono. Lakini hata baada ya kuwala wale wanono, mtu yeyote asingeweza kutambua kwamba wamewala wenzao, kwani bado walikuwa wamekondeana kama mwanzo. Hapo nikaamka usingizini. Kisha nikaota ndoto nyingine: Niliona masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka yakichipua katika bua moja. Halafu yakafuatwa na masuke mengine saba matupu, membamba na yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani. Yale masuke saba membamba yakayameza yale masuke saba mazuri. Basi, mimi niliwaambia wachawi ndoto hizo lakini hakuna mtu aliyeweza kunifafanulia.” Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto zako zote mbili tafsiri yake ni moja. Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni. Ngombe wale saba wazuri ni miaka saba, na yale masuke saba mazuri pia ni miaka saba; ndoto hiyo tafsiri yake ni moja. Wale ng'ombe saba waliokonda sana, ambao waliwafuata wale wanono, na yale masuke matupu saba, yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani, maana yake ni miaka saba ya njaa. Kama nilivyokueleza, ee Farao, Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni. Kutakuwa na miaka saba ya shibe katika nchi nzima ya Misri. Lakini baadaye itafuata miaka saba ya njaa, hata hiyo shibe isahaulike kabisa. Njaa hiyo itaiangamiza nchi hii. Shibe hiyo itasahaulika kabisa kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. Ndoto yako ilirudiwa mara mbili kwa mifano inayofanana kukuonesha kwamba Mungu ameamua, naye atatekeleza jambo hilo karibuni. “Kwa hiyo yafaa sasa, ee Farao, umteue mtu mwenye ujuzi na hekima, umpe jukumu la kuiangalia nchi yote ya Misri. Tena, ee Farao, uwateue wasimamizi kadhaa hapa nchini, uwaagize wakusanye sehemu ya tano ya mavuno yote ya Misri katika kipindi hiki cha miaka saba ya shibe. Uwaagize wasimamizi hao wakusanye chakula chote katika miaka saba ijayo ya mavuno kwa wingi. Nafaka hiyo na iwekwe chini ya mamlaka yako, ee Farao, iwe akiba ya chakula kwa miji yote, nao waitunze nafaka hiyo. Chakula hicho kitakuwa akiba ya kinga kwa nchi ya Misri isije ikaangamia kutokana na njaa ya miaka saba itakayofuata.” Shauri alilotoa Yosefu lilionekana kuwa jema mbele ya Farao na watumishi wake wote. Kwa hiyo Farao akawauliza watumishi wake, “Huyu mtu ana roho ya Mungu! Je, tunaweza kumpata mtu mwingine kama huyu?” Kisha akamwambia Yosefu, “Kwa kuwa Mungu amekufunulia haya yote, hakuna mtu mwingine mwenye busara na hekima kama wewe. Wewe ndiwe utakayeisimamia nchi yangu, na watu wangu wote watakuwa chini ya amri yako. Mimi tu ndiye mkuu kuliko wewe kwa kuwa nakalia kiti cha kifalme. Basi, sasa nakuteua rasmi kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri!” Ndipo, Farao akaivua pete yake ya mhuri kidoleni mwake na kumvisha Yosefu, akamvalisha na mavazi ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni. Farao akampandisha katika gari lake la pili la farasi na walinzi wakatangulia mbele ya Yosefu wakipaza sauti na kusema, “Pigeni magoti!” Ndivyo Farao alivyompa Yosefu madaraka makubwa juu ya nchi yote ya Misri. Zaidi ya hayo, Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ndimi Farao! Nasema: Mtu yeyote katika nchi nzima ya Misri asiinue mkono wala mguu wake bila kibali chako.” Farao akampa Yosefu jina la Kimisri: Safenath-panea. Akamwoza Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni. Basi, Yosefu akaanza kuitembelea nchi nzima ya Misri. Yosefu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kumtumikia Farao, mfalme wa Misri. Alitoka nyumbani kwa Farao na kuitembelea nchi yote ya Misri. Ikawa, katika miaka ile saba ya shibe, mashamba ya Misri yakatoa mazao kwa wingi sana. Yosefu akakusanya chakula chote wakati huo wa miaka saba ya shibe na kukiweka akiba katika miji ya Misri. Katika kila mji akaweka akiba ya chakula kutoka mashamba yaliyo karibu na mji huo. Yosefu akaweka akiba ya nafaka kwa wingi mno ikawa nyingi kama mchanga wa bahari, hata isiweze kupimika. Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Yosefu alikuwa amekwisha pata wana wawili kwa mkewe, Asenathi, binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni. Yosefu alimwita mwanawe wa kwanza Manase, akisema, “Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote na jamaa ya baba yangu.” Mwanawe wa pili akamwita Efraimu, akisema, “Mungu amenipa watoto katika nchi ya mateso yangu.” Miaka ile saba ya shibe nchini Misri ikapita. Ikaanza miaka saba ya njaa kama alivyokuwa amesema Yosefu hapo awali. Nchi nyingine zote zikawa na njaa, lakini nchi yote ya Misri ilikuwa na chakula. Wakati wananchi wa Misri walipoanza kuona njaa, walimlilia Farao awape chakula. Naye Farao akawaambia Wamisri wote, “Nendeni kwa Yosefu; atakalowaambia fanyeni.” Njaa ikazidi kuwa kali na kuenea katika nchi yote. Kwa hiyo Yosefu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri chakula. Zaidi ya hayo, watu toka kila mahali duniani walikuja Misri kwa Yosefu kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa kali duniani kote. Yakobo alipopata habari kwamba kulikuwa na nafaka huko Misri, aliwaambia wanawe, “Mbona mnaketi mkitazamana tu? Nimesikia kwamba Misri kuna nafaka. Nendeni huko mkanunue nafaka tusije tukafa njaa.” Hivyo ndugu kumi wa Yosefu wakaenda Misri kununua nafaka. Lakini Yakobo hakumwacha Benyamini, nduguye Yosefu, aende pamoja nao maana aliogopa kwamba angeweza kupata madhara. Basi, wana wa Israeli wakafika Misri wakiwa miongoni mwa wanunuzi wengine, kwani hata katika nchi ya Kanaani kulikuwa na njaa. Wakati huo Yosefu alikuwa ndiye mkuu huko Misri. Yeye ndiye aliyehusika na kuwauzia wananchi nafaka. Basi, kaka zake wakaja na kumwinamia Yosefu kwa heshima. Yosefu alipowaona kaka zake akawatambua, lakini akajifanya kana kwamba hawafahamu, akasema nao kwa ukali. Akawauliza, “Mmetoka wapi nyinyi?” Wakamjibu, “Tumetoka nchini Kanaani, tumekuja kununua chakula.” Ingawa Yosefu aliwatambua kaka zake, wao hawakumtambua. Akakumbuka ndoto zake za zamani juu ya kaka zake, akawaambia, “Nyinyi ni wapelelezi. Mmekuja kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.” Wao wakamjibu, “Sivyo, bwana wetu. Sisi watumishi wako tumekuja kununua chakula. Sisi ni ndugu, wana wa baba mmoja. Sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi.” Lakini Yosefu akasisitiza, “Sivyo! Mmekuja hapa ili kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.” Wakamwambia, “Sisi, watumishi wako, tuko ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja, mwenyeji wa nchi ya Kanaani. Mdogo wetu amebaki na baba nyumbani, na ndugu yetu mwingine ni marehemu.” Lakini Yosefu akawaambia, “Ni kama nilivyosema: Nyinyi ni wapelelezi tu. Hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Naapa kwa jina la Farao, kwamba hamtatoka hapa mpaka mdogo wenu atakapokuja. Mtumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu mdogo, wakati wengine wenu wanamngoja gerezani. Hapo ndipo maneno yenu yatakapojulikana ukweli wake. La sivyo, naapa kwa jina la Farao kwamba nyinyi ni wapelelezi.” Kisha akawatia wote gerezani kwa muda wa siku tatu. Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Kwa kuwa mimi ni mcha Mungu, fanyeni hivi ili mpate kuishi: Kama kweli nyinyi ni watu waaminifu, mmoja wenu na abaki kifungoni, na wengine wawapelekee nafaka jamaa zenu wenye njaa. Kisha mleteni kwangu ndugu yenu mdogo. Hii itathibitisha ukweli wa maneno yenu, nanyi hamtauawa.” Basi, wakakubali kufanya hivyo. Kisha wakasemezana wao kwa wao, “Kweli sisi tulimkosea ndugu yetu. Ingawa tulimwona akisononeka rohoni mwake, sisi hatukumjali hata alipotusihi. Ndiyo maana taabu hii yote inatupata.” Reubeni akawaambia, “Je, mimi sikuwaambieni tusimdhuru kijana? Lakini nyinyi hamkunisikiliza! Sasa tunaadhibiwa kwa ajili ya damu yake.” Wao hawakujua kuwa Yosefu alielewa yote hayo waliyosema, maana alipoongea nao ilikuwa kwa njia ya mkalimani. Yosefu akaenda kando, akaangua kilio. Alipotulia, akarudi kuzungumza nao. Kisha akamkamata Simeoni na kumtia pingu mbele ya macho yao. Yosefu akatoa amri mifuko yao ijazwe nafaka, kila mmoja wao arudishiwe fedha yake katika gunia lake, na wapewe chakula cha njiani. Wakafanyiwa mambo hayo yote. Wakawatwisha punda wao mizigo yao ya nafaka, wakaondoka. Ikawa walipofika mahali pa kulala wageni huko njiani, mmoja wao akafungua gunia lake ili apate kumlisha punda wake, akashangaa kukuta fedha yake mdomoni mwa gunia lake. Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Hii hapa mdomoni mwa gunia langu!” Waliposikia hayo, wakafa moyo. Wakatazamana huku wanatetemeka na kuulizana, “Ni jambo gani hili alilotutendea Mungu?” Walipowasili nchini Kanaani kwa baba yao Yakobo, walimsimulia yote yaliyowapata, wakamwambia, “Mkuu wa nchi ile alisema nasi kwa ukali, na kutushuku kwamba sisi ni wapelelezi nchini mwake. Lakini sisi tulimweleza kuwa sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi. Tulimweleza kuwa sisi tuko ndugu kumi na wawili wa baba mmoja, na kwamba mmoja wetu ni marehemu na yule mdogo yuko nyumbani nchini Kanaani pamoja na baba yetu. Ndipo mkuu wa nchi hiyo akatuambia, ‘Hivi ndivyo nitakavyotambua kama kweli nyinyi ni watu waaminifu: Mwacheni kwangu ndugu yenu mmoja, nanyi wengine mpeleke nafaka nyumbani kwa jamaa zenu wenye njaa. Kisha mleteni kwangu huyo ndugu yenu mdogo, na hapo nitajua kuwa nyinyi si wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Mkifanya hivyo nitamwacha huru ndugu yenu, nanyi mtaruhusiwa kufanya biashara katika nchi hii.’” Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka magunia yao, walishangaa kuona kila mmoja wao amerudishiwa kifuko chake na fedha ndani ya gunia lake. Walipoona hayo, wote pamoja na baba yao, wakashikwa na hofu. Baba yao Yakobo, akawaambia, “Mnanipokonya watoto wangu! Yosefu hayuko; Simeoni hayuko; sasa mnataka kumchukua na Benyamini. Yote hayo yamenipata!” Hapo Reubeni akamwambia baba yake, “Nisipomrudisha Benyamini, waue wanangu wawili. Mwache Benyamini mikononi mwangu, nami nitamlinda na kumrudisha kwako.” Lakini baba yake akamjibu, “Mwanangu hatakwenda nanyi; ndugu yake amekwisha fariki, naye peke yake ndiye aliyebaki. Mimi ni mzee mwenye mvi ikiwa kijana huyu atapatwa na madhara yoyote katika safari mtakayofanya basi, mtaniua kwa huzuni.” Kisha njaa ilizidi kuwa kali katika nchi ya Kanaani. Baada ya kile chakula walichokuwa wamenunua kutoka Misri kumalizika, Yakobo akawaambia wanawe, “Nendeni tena Misri, mkatununulie chakula kidogo.” Lakini Yuda akamwambia baba yake, “Yule mtu alituonya vikali, akisema, ‘Sitawapokea msipokuja na ndugu yenu mdogo.’ Kama utakubali ndugu yetu kwenda pamoja nasi, basi, tutakwenda kukununulia chakula. Lakini iwapo hutakubali aende nasi, basi, hatutakwenda huko, kwani yule mtu alituambia waziwazi, ‘Hamtaniona msipokuja na ndugu yenu mdogo.’” Israeli akasema, “Kwa nini mkanitia taabuni kwa kumwambia huyo mtu kwamba mnaye ndugu mwingine?” Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa makini sana kuhusu mambo yetu na jamaa yetu akisema, ‘Je, baba yenu angali hai? Je, mnaye ndugu mwingine?’ Hivyo tulimjibu kulingana na maswali yake. Tungaliwezaje kujua kwamba atatuambia, ‘Mleteni ndugu yenu?’” Yuda akamwambia Israeli, baba yake, “Niruhusu mimi niende naye ili tuondoke mara moja, tuende tukanunue chakula, tusije tukafa njaa pamoja nawe na watoto wetu. Mimi mwenyewe nitakuwa mdhamini wake. Wewe utanidai mimi. Nisipomrudisha ukamwona kwa macho yako mwenyewe, lawama na iwe juu yangu milele. Kama tusingalikawia, tungalikuwa tumekwisha kwenda na kurudi mara mbili.” Hapo Israeli, baba yao, akawaambia, “Haya! Kwa vile ni lazima iwe hivyo basi, fanyeni hivi: Chukueni katika mifuko yenu baadhi ya mazao bora ya nchi yetu, mkampelekee zawadi huyo mkuu. Mchukulieni mafuta kidogo ya mkwaju, asali kidogo, ubani, manemane, kungu na lozi. Chukueni fedha mara mbili ya ile inayohitajika, kwa sababu ni lazima mrudishe fedha ile iliyowekwa midomoni mwa magunia yenu; pengine ilirudishwa kwa makosa. Mchukueni pia ndugu yenu mwende kwa huyo mtu. Mungu Mwenye Nguvu na awajalieni kupata huruma mbele ya mtu huyo, awaachieni yule ndugu yenu mwingine na Benyamini warudi pamoja nanyi. Kwa upande wangu, ikinipasa kufiwa na wanangu basi!” Hapo, wakachukua zile zawadi, na fedha mara mbili ya zile za awali, wakaenda Misri pamoja na ndugu yao Benyamini. Walipowasili, wakaenda na kusimama mbele ya Yosefu. Yosefu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wapeleke watu hawa nyumbani, umchinje mnyama mmoja na kumtengeneza vizuri, maana watu hawa watakula nami chakula cha mchana.” Msimamizi huyo akafanya kama alivyoagizwa: Akawapeleka wale wageni nyumbani kwa Yosefu. Walipoona wamepelekwa nyumbani kwa Yosefu, wakashikwa na hofu, wakasema wao kwa wao, “Tumeletwa huku kwa sababu ya ile fedha tuliyorudishiwa katika magunia yetu tulipokuja safari ya kwanza ili apate kisingizio cha kutushambulia ghafla na kutunyanganya punda wetu na kutufanya watumwa wake.” Kwa hiyo wakamwendea yule msimamizi wa nyumba ya Yosefu wakaongea naye wakiwa mlangoni, wakamwambia, “Samahani, bwana! Sisi tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula. Tulipofika mahali pa kulala wageni huko njiani, tulifungua magunia yetu, tukashangaa kukuta fedha ya kila mmoja wetu mdomoni mwa gunia lake bila kuguswa. Sasa tumeirudisha fedha hiyo. Tumeleta na fedha nyingine kununulia chakula. Hatujui ni nani aliyeweka fedha yetu katika magunia yetu.” Yule msimamizi akawajibu, “Msiwe na wasiwasi, wala msiogope. Bila shaka Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, ndiye aliyewarudishieni fedha katika magunia yenu. Mimi nilipokea fedha yenu.” Kisha akawaletea Simeoni, ndugu yao. Huyo msimamizi alipowakaribisha nyumbani kwa Yosefu, akawapa maji ya kunawa miguu yao, na punda wao akawalisha. Nao wakatayarisha zawadi zao za kumpa Yosefu, kwa sababu walisikia kuwa watakula pamoja naye. Yosefu, aliporudi nyumbani, wakamletea zile zawadi walizokuwa nazo, wakamwinamia kwa heshima. Yosefu akawauliza habari zao na kusema, “Mlinisimulia habari za mzee, baba yenu. Je, hajambo? Angali hai?” Wakamjibu, “Mtumishi wako, baba yetu, hajambo na angali hai.” Kisha wakainama kwa heshima. Yosefu alipoinua macho yake na kumwona Benyamini, nduguye, mtoto wa mama yake, akasema, “Huyu ndiye ndugu yenu mdogo mliyeniambia habari zake? Mungu na akufadhili, mwanangu!” Ghafla, Yosefu akatoka mahali hapo, kwani machozi yalikuwa yanamlengalenga kwa shauku kubwa juu ya ndugu yake, akaingia chumbani mwake na kuangua kilio. Baada ya kunawa uso wake, alitoka huku akijikaza, akaamuru chakula kiletwe. Yosefu aliandaliwa chakula chake peke yake, na ndugu zake wakaandaliwa peke yao, hali kadhalika na Wamisri waliokula pamoja naye, wakaandaliwa peke yao, kwani ni chukizo kwa Wamisri kula chakula pamoja na Waebrania. Ndugu zake Yosefu waliketi mbele yake kulingana na umri wao, kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho, wakawa wanaangaliana kwa mshangao. Chakula kilikuwa kikichukuliwa kutoka mezani pa Yosefu na kupelekwa kwao, lakini Benyamini alipewa mara tano zaidi ya kiasi walichopewa ndugu zake. Basi, wakanywa na kufurahi pamoja naye. Kisha Yosefu alimwagiza msimamizi wa nyumba yake akisema, “Yajaze magunia ya watu hawa nafaka kiasi watakachoweza kuchukua. Halafu, weka fedha ya kila mmoja wao mdomoni mwa gunia lake. Katika gunia la yule mdogo kabisa, kiweke kile kikombe changu cha fedha, pamoja na fedha yake.” Huyo msimamizi akafanya kama alivyoamriwa na Yosefu. Kulipopambazuka wakaruhusiwa kuondoka pamoja na punda wao. Walipokuwa wamesafiri mwendo mfupi tu kutoka mjini, Yosefu alimwambia msimamizi wa nyumba yake, “Haraka! Wafuate wale watu, na utakapowakuta, uwaulize, ‘Kwa nini mmelipa mema mliyotendewa kwa maovu? Kwa nini mmeiba kikombe cha bwana wangu ambacho yeye hunywa nacho na kukitumia kupiga ramli? Mmekosa sana kwa kufanya hivyo!’” Yule msimamizi alipowakuta akawaambia maneno haya. Lakini wao wakamwuliza, “Bwana, una maana gani kutuambia maneno kama hayo? Sisi watumishi wako kamwe hatuwezi kufanya jambo kama hilo! Kumbuka, bwana, fedha tuliyokuta katika midomo ya magunia yetu tuliirudisha kutoka katika nchi ya Kanaani. Itawezekanaje tena tuibe fedha au dhahabu nyumbani mwa bwana wako? Basi, kama akipatikana mmoja wetu ana kikombe hicho, na auawe, na sisi wengine wote tutakuwa watumwa wako.” Huyo msimamizi akasema, “Sawa; na iwe kama mlivyosema. Yeyote atakayepatikana na kikombe hicho, atakuwa mtumwa wangu, lakini wengine wote hamtakuwa na lawama.” Basi, kila mmoja akashusha gunia lake chini haraka na kulifungua. Yule msimamizi akayapekua magunia yote, akianzia la mkubwa wao na kumalizia na la mdogo kabisa. Kikombe kikapatikana katika gunia la Benyamini. Hapo wakayararua mavazi yao kwa huzuni. Kila mmoja wao akambebesha punda wake mzigo wake, wakarudi mjini. Yuda na nduguze wakafika nyumbani kwa Yosefu naye Yosefu alikuwapo bado nyumbani. Basi, wakamwinamia kwa heshima, naye Yosefu akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivyo? Je hamjui kwamba mtu kama mimi ninao uwezo wa kubashiri?” Yuda akamjibu, “Tukuambie nini bwana? Tuseme nini kuonesha kwamba hatuna hatia? Mungu ameyafichua makosa yetu, sisi watumishi wako. Sasa sote tu watumwa wako, sisi pamoja na yule aliyepatikana na kikombe chako.” Lakini Yosefu akasema, “La! Mimi siwezi kufanya hivyo! Yule tu aliyepatikana na kikombe changu ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nyinyi wengine wote rudini kwa amani kwa baba yenu.” Ndipo Yuda akamkaribia Yosefu na kumwambia, “Bwana, nakuomba uniruhusu mimi mtumishi wako, nijitetee mbele yako kwa maneno machache; ninakusihi usinikasirikie, kwani wewe ni kama Farao mwenyewe. Bwana, wewe ulituuliza kama tuna baba au ndugu, nasi tukakueleza kwamba tunaye baba, naye ni mzee, na kwamba tunaye ndugu mwingine mdogo aliyezaliwa wakati wa uzee wa baba yetu. Kaka yake huyo kijana amekwisha fariki, na huyo mdogo ndiye peke yake aliyebaki wa mama yake; na mzee wetu anampenda sana kijana huyo. Bwana, ulituagiza sisi watumishi wako kumleta huyo mdogo wetu upate kumwona. Tukakueleza kwamba huyo kijana hawezi kuachana na baba yake, kwa sababu akifanya hivyo baba yake atakufa. Lakini wewe bwana ukatuambia kwamba kama hatutakuja na ndugu yetu mdogo, hutatupokea tena. “Tuliporudi nyumbani kwa mtumishi wako, baba yetu, tulimwarifu ulivyotuagiza, bwana. Naye alipotuambia tuje tena huku kununua chakula, tulimwambia, ‘Hatuwezi kwenda, isipokuwa tu kama ndugu yetu mdogo atakwenda pamoja nasi; kama hatakwenda pamoja nasi hatuwezi kupokelewa na yule mtu.’ Basi, baba yetu, mtumishi wako, akatuambia, ‘Mnajua kwamba mke wangu Raheli alinizalia wana wawili: Mmoja alitoweka, nami nikasema, bila shaka ameraruliwa vipandevipande na mnyama wa porini, maana sijapata kumwona tena. Kama mtamchukua huyu pia kutoka kwangu, akipatwa na madhara basi, mtanishusha kuzimu nikiwa mzee mwenye huzuni.’ Kwa hiyo basi, bwana, nikimrudia baba yangu mtumishi wako bila kijana huyu, na hali uhai wa baba unategemea uhai wa kijana huyu, akiona kwamba kijana hayupo pamoja nasi, atakufa! Hivyo sisi watumishi wako, tutamuua baba yetu kwa huzuni. Zaidi ya hayo, mimi binafsi nilijitoa kuwa mdhamini wa huyu kijana kwa baba yangu, nikisema, ‘Nisipomrudisha Benyamini kwako, lawama na iwe juu yangu milele.’ Sasa, ee bwana, nakusihi, mimi mtumishi wako, nibaki, niwe mtumwa wako badala ya kijana huyu. Mwache yeye arudi nyumbani pamoja na ndugu zake. Nitawezaje kumrudia baba yangu bila kijana huyu? Siwezi kustahimili kuyaona madhara yatakayompata baba yangu.” Hapo Yosefu akashindwa kujizuia mbele ya wote walioandamana naye, akawaamuru watoke nje. Hivyo Yosefu alikuwa peke yake alipojitambulisha kwa ndugu zake. Lakini alilia kwa sauti kubwa hata Wamisri wakamsikia, hali kadhalika na watu wa jamaa ya Farao nao wakamsikia. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu. Je, baba yangu angali hai?” Lakini ndugu zake wakapigwa na bumbuazi mbele yake, hata wakashindwa kumjibu. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, sogeeni karibu nami.” Walipomkaribia, akawaambia, “Mimi ndiye ndugu yenu Yosefu, mliyemwuza Misri. Lakini sasa msifadhaike wala kujilaumu kwa kuniuza. Mungu ndiye aliyenileta huku niwatangulie, ili niyaokoe maisha ya watu. Huu ni mwaka wa pili tu wa njaa nchini, na bado kuna miaka mitano zaidi ambapo watu hawataweza kulima wala kuvuna mavuno. Mungu alinileta huku niwatangulie, ili kusalimisha maisha yenu mbaki hai nchini na kuwakomboa kwa ukombozi mkubwa. Kwa hiyo, si nyinyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Ndiye aliyenifanya kama baba kwa Farao, msimamizi wa nyumba yake yote na mtawala wa nchi yote ya Misri. Basi, fanyeni haraka, mwende kwa baba na kumwambia, ‘Yosefu, mwana wako, anasema: Mungu amenifanya kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri. Basi, usikawie kuja kwangu. Utakaa karibu nami katika eneo la Gosheni: Wewe, wana wako na wajukuu wako, mifugo yako na mali yako yote. Utakapokuwa Gosheni, mimi nitakutunza wewe, jamaa yako pamoja na mifugo yako ili msije mkafa njaa, kwani bado miaka mitano zaidi ya njaa.’” Kisha Yosefu akasema, “Nyinyi wenyewe mmeona kwa macho yenu na hata ndugu yangu Benyamini ameona kwa macho yake kwamba ni mimi mwenyewe Yosefu ninayezungumza nanyi. Ni lazima kumwambia baba yangu juu ya fahari yangu huku Misri na yote mliyoyaona. Basi, fanyeni haraka, mkamlete baba yangu huku.” Kisha Yosefu akamkumbatia Benyamini, nduguye, akalia; Benyamini naye akalia, huku wamekumbatiana. Akiwa bado analia, Yosefu akawakumbatia ndugu zake na kuwabusu. Hapo ndipo ndugu zake walipoweza kuzungumza naye. Habari hizo zilipofika ikulu ya mfalme, kwamba ndugu za Yosefu wamekuja, zikamfurahisha sana Farao na watumishi wake. Kwa hiyo, Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako wawapakie punda wao mizigo, warudi nchini Kanaani, wamlete hapa baba yao na jamaa zao wote. Mimi nitawapa sehemu nzuri kabisa ya nchi ya Misri, ambako wataweza kufurahia matunda yote ya nchi hii. Waambie pia wachukue kutoka hapa magari ya kukokotwa ya kuwaleta watoto wao wachanga na wake zao na wala wasikose kumleta baba yao. Waambie wasijali juu ya mali zao maana sehemu nzuri kuliko zote katika nchi ya Misri itakuwa yao.” Basi, wana wa Israeli wakafanya kama walivyoagizwa. Yosefu akawapa magari kulingana na maagizo ya Farao na chakula cha njiani. Aliwapa kila mmoja wao mavazi ya kubadili, lakini akampa Benyamini vipande 300 vya fedha na mavazi matano ya kubadili. Tena alimpelekea baba yake zawadi hizi kwa ajili ya safari yake: Punda kumi waliobeba bidhaa bora za Misri, punda jike kumi waliobeba nafaka, mikate na vyakula vingine. Basi, Yosefu akaagana na ndugu zake. Walipokuwa wanaondoka aliwaonya akisema, “Msigombane njiani!” Basi, wakatoka Misri na kurudi nyumbani kwa baba yao Yakobo, nchini Kanaani. Wakamwambia baba yao, “Yosefu yu hai! Yeye ndiye mtawala wa nchi yote ya Misri!” Hapo baba yao akapigwa na bumbuazi, kwani hakuweza kuyasadiki maneno yao. Lakini, walipomsimulia yote waliyoagizwa na Yosefu na alipoyaona magari aliyopelekewa na Yosefu kumchukua, moyo wake ukajaa furaha kupita kiasi. Israeli akasema, “Sasa nimeridhika; mwanangu Yosefu yu hai! Nitakwenda nimwone kabla sijafa.” Basi, Israeli akaanza safari yake pamoja na mali yake yote. Alipofika Beer-sheba, akamtolea tambiko Mungu wa Isaka, baba yake. Mungu akaongea na Israeli katika maono usiku, akamwita, “Yakobo! Yakobo!” Yakobo akaitika, “Naam nasikiliza.” Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu, Mungu wa baba yako. Usiogope kwenda Misri; utakapokuwa huko, nitakufanya uwe taifa kubwa. Mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nawe huko Misri na kukurudisha huku. Utakapofariki, mkono wa Yosefu ndio utakaoyafumba macho yako.” Basi, Yakobo akaondoka Beer-sheba. Wanawe wakamchukua yeye, watoto wao wachanga pamoja na wake zao katika magari ambayo Farao alipeleka kumchukua. Walichukua pia mifugo na mali yao yote waliyokuwa wamechuma katika nchi ya Kanaani, wakaenda Misri. Yakobo aliwachukua wazawa wake wote: Wanawe, wajukuu wake wa kiume na wa kike, wote akawaleta Misri. Wazawa wa Israeli ambao walikwenda Misri pamoja naye walikuwa Reubeni, mzaliwa wake wa kwanza, pamoja na wana wa Reubeni: Henoki, Palu, Hesroni na Karmi. Simeoni na wanawe: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli, aliyezaliwa na mwanamke Mkanaani. Lawi na wanawe: Gershoni, Kohathi na Merari. Yuda na wanawe: Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera. (Lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani). Wana wa Peresi walikuwa Hesroni na Hamuli. Isakari na wanawe: Tola, Puva, Yashubu na Shimroni. Zebuluni na wanawe: Seredi, Eloni na Yaleeli. Hao ndio wana ambao Lea alimzalia Yakobo kule Padan-aramu, pamoja na Dina binti yake. Jumla ya wanawe, binti zake na wajukuu wake walikuwa watu thelathini na watatu. Gadi na wanawe: Sifioni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli. Asheri na wanawe: Imna, Ishva, Ishvi, Beria na Sera, dada yao. Beria na wanawe: Heberi na Malkieli. Hawa kumi na sita ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Zilpa, mjakazi ambaye Labani alimpa Lea, binti yake. Raheli alimzalia Yakobo wana wawili: Yosefu na Benyamini. Huko Misri, Asenathi, binti Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yosefu wana wawili: Manase na Efraimu. Wana wa Benyamini walikuwa Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi. Watu hao kumi na wanne ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Raheli, mkewe. Dani na Hushimu, mwanawe. Naftali na wanawe: Yaseeli, Guni, Yeseri na Shilemu. Hao saba ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Bilha, mjakazi ambaye Labani alimpa binti yake Raheli. Jumla ya wazawa wa Yakobo aliokwenda nao Misri, bila kuwahesabu wake za wanawe, ilikuwa watu sitini na sita. Huko nchini Misri Yosefu alikuwa amepata wana wawili. Kwa hiyo watu wote wa jamaa ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini. Yakobo akamtanguliza Yuda kwa Yosefu kumwomba waonane huko Gosheni; nao wakafika katika eneo la Gosheni. Yosefu akapanda gari lake la farasi, akaenda kumlaki Israeli, baba yake, huko Gosheni. Alipomfikia baba yake, alimkumbatia na kulia kwa kitambo kirefu. Israeli akamwambia Yosefu, “Hata nikifa sasa si kitu kwa kuwa nimeuona uso wako na kujua kwamba wewe u hai!” Yosefu akawaambia ndugu zake na jamaa yote ya baba yake, “Nakwenda kumwarifu Farao kwamba ndugu zangu na jamaa yote ya baba yangu waliokuwa katika nchi ya Kanaani wamekuja kwangu. Nitamweleza kwamba nyinyi ni wachungaji kwani mmekuwa mkichunga mifugo, na kwamba mmewasili pamoja na mbuzi, kondoo, ng'ombe na mali yenu yote. Basi, Farao akiwaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’ Semeni: ‘Bwana, sisi watumishi wako, ni wafugaji wa mifugo tangu utoto wetu mpaka leo, kwani ndivyo walivyokuwa babu zetu’; semeni hivyo ili mruhusiwe kukaa katika eneo la Gosheni.” Yosefu alisema hivyo kwa sababu kwa Wamisri wachungaji wote wa kondoo ni chukizo. Basi, Yosefu akaenda kwa Farao, akamwambia, “Baba yangu na ndugu zangu pamoja na kondoo, ng'ombe na mali yao yote, wamefika kutoka nchi ya Kanaani. Sasa wako katika eneo la Gosheni.” Yosefu alikuwa amewachukua ndugu zake watano, akawajulisha kwa Farao. Farao akawauliza, “Kazi yenu ni nini?” Wakamjibu, “Bwana, sisi watumishi wako ni wachungaji, kama walivyokuwa babu zetu.” Kisha wakamwambia Farao, “Sisi watumishi wako tumekuja kukaa kama wageni humu nchini kwa kuwa njaa ni kali huko Kanaani na hakuna tena malisho kwa mifugo yetu. Hivyo, bwana, tunakuomba, sisi watumishi wako, uturuhusu kukaa katika eneo la Gosheni.” Farao akamwambia Yosefu, “Baba yako na ndugu zako wamekujia wewe. Nchi yote ya Misri iko chini yako; wape baba yako na ndugu zako sehemu bora ya nchi hii. Waache wakae katika eneo la Gosheni. Na iwapo unawafahamu watu stadi miongoni mwao, wateue wawe waangalizi wa mifugo yangu.” Kisha, Yosefu akamleta baba yake Yakobo kumwamkia Farao; naye Yakobo akampa Farao baraka zake. Farao akamwuliza Yakobo, “Umri wako ni miaka mingapi?” Yakobo akamjibu, “Umri niliojaliwa kama msafiri ni miaka 130. Miaka hiyo imekuwa michache na iliyojaa mateso, tena haijafikia idadi ya miaka waliyoishi wazee wangu kama wasafiri.” Kisha Yakobo akambariki Farao, akaondoka. Basi, Yosefu akawapa baba yake na ndugu zake eneo la Ramesesi lililo bora kabisa katika nchi ya Misri, liwe makao yao, nao wakalimiliki kama alivyoagiza Farao. Yosefu akawa anawapatia chakula baba yake, ndugu zake na jamaa yote ya baba yake kulingana na idadi ya watu waliowategemea. Baadaye chakula kiliadimika kabisa nchini kote. Njaa ilikuwa kali sana hata ikawafanya watu wote katika nchi ya Misri na ya Kanaani kudhoofika. Yosefu akakusanya fedha yote ya nchi ya Misri na Kanaani kutokana na nafaka waliyonunua, akaipeleka fedha hiyo ikulu kwa Farao. Baada ya watu wote wa nchi ya Misri na Kanaani kutumia fedha yao yote Wamisri wote walimjia Yosefu na kumwambia, “Tupe chakula! Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Tazama, sasa fedha yetu imekwisha!” Yosefu akawaambia, “Kama fedha yenu imekwisha, basi nipeni mifugo yenu, nami nitawapa nafaka.” Ndipo wakamletea Yosefu mifugo yao: Farasi, ng'ombe, kondoo, mbuzi na punda, naye akawapa chakula. Mwaka huo Yosefu akawa anawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote. Mwaka uliofuata wakamjia tena na kumwambia, “Bwana, ukweli ni kwamba fedha yetu yote imekwisha, na wanyama wetu wamekuwa mali yako. Sasa, bwana, sisi watumishi wako hatuna chochote tunachoweza kukupa isipokuwa miili yetu na mashamba yetu. Ya nini sisi tufe mbele ya macho yako na mashamba yetu yaharibike? Utununue sisi pamoja na mashamba yetu, tuwe watumwa wa Farao, mradi tu utupe chakula. Tupe nafaka, tusije tukafa; utupe na mbegu kwa ajili ya mashamba yetu.” Hivyo Yosefu akainunua nchi yote ya Misri iwe mali ya Farao. Kila Mmisri alilazimika kuuza shamba lake, kwa jinsi njaa ilivyokuwa kali. Nchi yote ikawa mali ya Farao, na Yosefu akawafanya watu kuwa watumwa, kutoka pembe moja hadi pembe nyingine ya nchi ya Misri. Ardhi ambayo Yosefu hakuinunua ni ile iliyomilikiwa na makuhani. Hao hawakulazimika kuiuza ardhi yao kwani waliishi kwa posho maalumu waliyopewa na Farao. Kisha Yosefu akawaambia watu, “Tazameni, nimekwisha wanunua nyinyi nyote na mashamba yenu kuwa mali ya Farao. Mtapewa mbegu nanyi mtapanda mashamba yenu. Wakati wa mavuno, sehemu moja ya tano mtampa Farao. Sehemu nne zitakazobaki zitakuwa mbegu na chakula kwa ajili yenu na jamaa zenu na watoto wenu.” Wakamjibu, “Bwana, umeyaokoa maisha yetu! Kwa vile umetuonesha wema wako, sisi tutakuwa watumwa wa Farao.” Ndivyo Yosefu alivyotangaza sheria moja ambayo iko mpaka leo nchini Misri: Kila raia lazima atoe sehemu moja ya tano ya mavuno yake kwa Farao. Ardhi ya makuhani tu ndiyo haikununuliwa na kufanywa mali ya Farao. Basi, watu wa Israeli wakakaa katika eneo la Gosheni nchini Misri. Wakiwa huko, wakachuma mali nyingi, wakazaana na kuongezeka sana. Yakobo alikaa katika nchi ya Misri kwa muda wa miaka kumi na saba, hadi alipofikia umri wa miaka 147. Wakati wa kufa kwake ulipokaribia, Yakobo akamwita mwanawe Yosefu, akamwambia, “Sasa, kama kweli unanipenda, weka mkono wako mapajani mwangu, uniahidi kwamba utanitendea kwa heshima na haki. Usinizike huku Misri, ila unilaze pamoja na babu zangu. Nichukue kutoka Misri, ukanizike katika makaburi yao.” Yosefu akamjibu, “Nitafanya kama ulivyosema.” Yakobo akamwambia, “Niapie!” Yosefu akamwapia. Kisha Israeli akainamia upande wa kichwa cha kitanda chake. Baada ya hayo, Yosefu alipewa habari kwamba baba yake ni mgonjwa. Hivyo, akawachukua wanawe wawili, Manase na Efraimu, akaenda nao kwa baba yake. Yakobo alipofahamishwa kwamba mwanawe Yosefu amefika kumwona, akajitahidi kuinuka, akaketi kitandani. Yakobo akamwambia Yosefu, “Mungu mwenye nguvu alinitokea nilipokuwa kule Luzu katika nchi ya Kanaani, akanibariki. Aliniambia, ‘Tazama, nitakufanya uwe na wazawa na uongezeke; nitakufanya uwe babu wa jamii kubwa za watu. Ardhi hii nitawapa wazawa wako, waimiliki milele.’” Yakobo akaendelea kusema, “Wanao wawili uliowapata hapa Misri kabla sijafika, ni wanangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu kama walivyo Reubeni na Simeoni. Lakini, watoto utakaopata baadaye watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao. Naamua hivyo kwa sababu ya mama yako, Raheli. Nilipokuwa narudi kutoka Padani yeye alifariki katika nchi ya Kanaani, tukiwa karibu kufika Efratha, akaniachia huzuni. Basi, nikamzika papo hapo, kando ya njia iendayo Efratha, yaani Bethlehemu.” Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akamwuliza, “Ni akina nani hawa?” Yosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wanangu alionijalia Mungu nikiwa huku.” Israeli akasema, “Tafadhali, walete karibu nipate kuwabariki.” Macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee. Basi, Yosefu akawasogeza wanawe karibu na baba yake, naye akawabusu na kuwakumbatia. Kisha Israeli akamwambia Yosefu, “Sikutazamia kuuona uso wako tena; lakini, kumbe, Mungu amenijalia hata kuwaona watoto wako!” Hapo Yosefu akawaondoa wanawe kwenye magoti ya baba yake, kisha akainama kwa heshima. Yosefu akawainua wanawe wawili, Efraimu katika mkono wake wa kulia, akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa baba yake, na Manase katika mkono wake wa kushoto, akimwelekeza kwenye mkono wa kulia wa baba yake, akawasogeza kwa babu yao. Lakini Israeli akaipishanisha mikono yake: Mkono wake wa kulia akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, aliyekuwa mzaliwa wa kwanza. Kisha Israeli akambariki Yosefu, akisema, “Mungu ambaye babu zangu Abrahamu na Isaka walimtii maishani mwao, Mungu ambaye ameniongoza maishani mwangu hadi leo, na malaika ambaye aliniokoa katika mabaya yote, na awabariki vijana hawa! Jina langu na majina ya wazee wangu, Abrahamu na Isaka, yadumishwe katika vijana hawa; nao waongezeke kwa wingi duniani.” Yosefu alipoona kwamba baba yake ameuweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa cha Efraimu hakupendezwa. Basi, akaushika mkono wa baba yake, akitaka kuuondoa juu ya kichwa cha Efraimu auweke juu ya kichwa cha Manase. Akamwambia baba yake, “Sivyo, baba! Huyu hapa ndiye mzaliwa wa kwanza. Tafadhali, uweke mkono wako wa kulia juu ya kichwa chake.” Lakini baba yake akakataa, akisema, “Najua, mwanangu, najua. Wana wa Manase pia watakuwa taifa kubwa na mashuhuri. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, na wazawa wake watakuwa mataifa mengi.” Basi, Israeli akawabariki siku hiyo, akisema, “Waisraeli watayatumia majina yenu kubarikia, watasema, ‘Mungu akutendee mema kama Efraimu na Manase!’” Ndivyo Israeli alivyomweka Efraimu mbele ya Manase. Kisha Israeli akamwambia Yosefu, “Kama uonavyo, mimi niko karibu kufa. Hata hivyo, Mungu atakuwa pamoja nanyi, na kuwarudisheni katika nchi ya babu zenu. Zaidi ya hayo, nimekupa wewe, wala si ndugu zako, eneo moja milimani, nililowanyanganya Waamori kwa upanga na upinde wangu.” Yakobo akawaita wanawe, akasema, “Kusanyikeni pamoja niwaambieni mambo yatakayowapata siku zijazo. “Kusanyikeni msikie, enyi wana wa Yakobo, nisikilizeni mimi Israeli, baba yenu. “Wewe Reubeni ni mzaliwa wangu wa kwanza, nguvu yangu na tunda la ujana wangu. Wewe wawapita ndugu zako kwa ukuu na nguvu. “Wewe ni kama maji ya mafuriko. Lakini hutakuwa wa kwanza tena, maana ulipanda kitandani mwangu mimi baba yako, wewe ulikitia najisi; naam wewe ulikipanda! “Simeoni na Lawi ni ndugu: Silaha zao wanatumia kufanya ukatili, lakini mimi sitashiriki njama zao; ee roho yangu, usishiriki mikutano yao, maana, katika hasira yao, walimuua mtu, kwa utundu wao walikata mshipa wa ng'ombe. “Nalaani hasira yao maana ni kali mno, na ghadhabu yao isiyo na huruma. Nitawatawanya katika nchi ya Yakobo, nitawasambaza katika nchi ya Israeli. “Wewe Yuda, ndugu zako watakusifu. Adui zako utawakaba shingo; na ndugu zako watainama mbele yako. “Wewe Yuda, mwanangu, ni kama mwanasimba ambaye amepata mawindo yake akapanda juu. Kama simba hujinyosha na kulala chini; simba mwenye nguvu, nani athubutuye kumwamsha? “Fimbo ya kifalme haitatoka kwa Yuda, wala bakora ya utawala miguuni pake, mpaka atakapofika yule ambaye ni yake; ambaye mataifa yatamtii. “Atafunga punda wake katika mzabibu na mwanapunda wake kwenye mzabibu bora. Hufua nguo zake katika divai, na mavazi yake katika divai nyekundu. “Macho yake ni mekundu kwa divai, meno yake ni meupe kwa maziwa. “Zebuluni ataishi sehemu za pwani, pwani yake itakuwa mahali pa kuegesha meli. Nchi yake itapakana na Sidoni. “Isakari ni kama punda mwenye nguvu, ajilazaye kati ya mizigo yake. “Aliona kuwa mahali pa kupumzikia ni pema, na kwamba nchi ni ya kupendeza, akauinamisha mgongo wake kubeba mzigo, akawa mtumwa kufanya kazi za shuruti. “Dani atakuwa mwamuzi wa watu wake, kama mojawapo ya makabila ya Israeli. “Atakuwa kama nyoka njiani, nyoka mwenye sumu kando ya njia, aumaye visigino vya farasi, naye mpandafarasi huanguka chali. “Ee Mwenyezi-Mungu, nangojea uniokoe! “Gadi atashambuliwa na wanyanganyi, lakini yeye atawafuata nyuma na kuwashambulia. “Ardhi ya Asheri itatoa mavuno kwa wingi, naye atatoa chakula kimfaacho mfalme. “Naftali ni kama paa aliye huru, azaaye watoto walio wazuri. “Yosefu ni kama mti uzaao, mti uzaao kando ya chemchemi, matawi yake hutanda ukutani. “Wapiga mishale walimshambulia vikali, wakamtupia mishale na kumsumbua sana. “Lakini upinde wake bado imara, na mikono yake imepewa nguvu, kwa uwezo wa Mwenye Nguvu wa Yakobo, kwa jina la Mchungaji, Mwamba wa Israeli; “kwa Mungu wa baba yako atakayekusaidia, kwa Mungu mwenye nguvu atakayekubariki; upate baraka za mvua toka juu mbinguni, baraka za maji ya vilindi vilivyo chini, baraka za uzazi wa akina mama na mifugo. Baraka za baba yako zishinde baraka za milima ya milele, ziwe bora kuliko vilima vya kale. Baraka hizo na ziwe juu ya kichwa cha Yosefu, juu ya paji lake yeye aliyekuwa ametengwa na ndugu zake. “Benyamini ni mbwamwitu mkali; asubuhi hula mawindo yake, na jioni hugawa nyara.” Hayo ndiyo makabila kumi na mawili ya Israeli, na hayo ndiyo maneno aliyowaambia baba yao alipowabariki, kila mmoja wao kama alivyostahili. Kisha Israeli akawaagiza wanawe hivi, “Mimi karibu nife na kujiunga na watu wangu. Nizikeni pamoja na wazee wangu katika pango lililoko shambani mwa Efroni Mhiti, kule Makpela, mashariki ya Mamre, nchini Kanaani. Abrahamu alinunua pango na shamba hilo kwa Efroni, Mhiti, liwe lake la kuzikia. Huko ndiko walikozikwa Abrahamu na mkewe Sara; huko ndiko walikozikwa Isaka na mkewe Rebeka; na huko ndiko nilikomzika Lea. Shamba hilo na pango lake lilinunuliwa kwa Wahiti.” Yakobo alipomaliza kuwausia wanawe, aliirudisha miguu yake kitandani, akatoa roho akajiunga na wazee wake. Hapo Yosefu akamkumbatia baba yake akilia na kumbusu. Kisha, akawaagiza waganga wake wampake Israeli, baba yake, dawa ili asioze, nao wakafanya hivyo. Kama kawaida, siku arubaini zilihitajika kwa kazi hiyo. Wamisri nao wakaomboleza kifo cha Yakobo kwa muda wa siku sabini. Baada ya matanga kumalizika, Yosefu akawaambia watu wa jamaa ya Farao, “Ikiwa nimekubalika mbele yenu, tafadhali zungumzeni na Farao kwa niaba yangu kwamba baba yangu aliniapisha, akisema, ‘Mimi karibu nitafariki. Yakupasa kunizika katika kaburi nililojichongea katika nchi ya Kanaani.’ Kwa hiyo namwomba aniruhusu niende kumzika baba yangu, kisha nitarudi.” Farao akajibu, “Nenda ukamzike baba yako kama alivyokuapisha.” Basi, Yosefu akaondoka kwenda kumzika baba yake akifuatana na watumishi wote wa Farao, wazee wa nyumba ya Farao, pamoja na wazee wa nchi nzima ya Misri. Hali kadhalika, Yosefu alifuatana na jamaa yake yote, ndugu zake na jamaa yote ya baba yake Yakobo. Katika eneo la Gosheni walibaki watoto wao tu pamoja na kondoo, mbuzi na ng'ombe wao. Pia waliandamana naye wapandafarasi na magari; lilikuwa kundi kubwa sana. Walipofika katika uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, ngambo ya mto Yordani, waliomboleza kwa huzuni kubwa, naye Yosefu akamfanyia baba yake marehemu matanga ya siku saba. Wakanaani wenyeji wa nchi hiyo, walipoyaona maombolezo yaliyofanywa kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, wakasema, “Maombolezo haya ya Wamisri, kweli ni makubwa!” Kwa hiyo, mahali pale pakaitwa Abel-misri, napo pako ngambo ya mto Yordani. Wana wa Yakobo walimfanyia baba yao kama alivyowaagiza: Walimchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika katika pango lililokuwa katika shamba kule Makpela, mashariki ya Mamre. Pango pamoja na shamba hilo Abrahamu alikuwa amelinunua kwa Efroni Mhiti, ili pawe mahali pake pa kuzikia. Baada ya kumzika baba yake, Yosefu alirudi Misri pamoja na ndugu zake na watu wote waliokuwa wameandamana naye kwenda kumzika baba yake. Baada ya kifo cha baba yao, ndugu zake Yosefu walisemezana, “Huenda Yosefu atatuchukia na kutulipiza mabaya yote tuliyomtendea.” Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakisema, “Baba yako, kabla hajafariki, aliagiza hivi, ‘Mwambieni Yosefu kwa niaba yangu: Tafadhali uwasamehe ndugu zako makosa yao mabaya na maovu yote waliyokutendea.’ Sasa basi, tafadhali usamehe uovu tuliokutendea sisi watumishi wa Mungu wa baba yako.” Yosefu alipopata ujumbe huu, alilia. Kisha ndugu zake wakamjia, wakainama mpaka chini mbele yake, wakasema, “Tazama, sisi tu watumishi wako.” Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope, je, mimi ni badala ya Mungu? Nyinyi mlitaka kunitendea vibaya, lakini Mungu alikusudia mema ili watu wengi wapate kuwa hai kama mwonavyo leo. Haya, msiogope. Mimi nitawapeni chakula pamoja na watoto wenu.” Basi akawafariji na kusema nao vizuri. Yosefu akaendelea kukaa katika nchi ya Misri pamoja na jamaa yote ya baba yake. Aliishi kwa muda wa miaka 110. Yosefu alijaliwa kuwaona watoto na wajukuu wa mwanawe Efraimu, na pia kuwapokea kama wanawe watoto wa Makiri mwana wa Manase. Baadaye Yosefu aliwaambia ndugu zake, “Mimi sasa ninakaribia kufa. Lakini Mungu hakika atawajia kuwasaidia. Atawatoa katika nchi hii na kuwapelekeni katika nchi aliyowaapia Abrahamu, Isaka na Yakobo.” Kisha Yosefu akawaapiza wana wa Israeli, akisema, “Mungu atakapowajia kuwasaidia, hakikisheni kwamba mmeichukua mifupa yangu kutoka huku.” Basi, Yosefu akafariki kule Misri, akiwa na umri wa miaka 110. Nao wakaupaka mwili wake dawa usioze, wakauweka katika jeneza kule Misri. Haya ndiyo majina ya watoto wa kiume wa Israeli, ambao walikwenda Misri, kila mmoja na jamaa yake: Reubeni, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Zebuluni, Benyamini, Dani, Naftali, Gadi na Asheri. Wazawa wote wa Yakobo walikuwa watu 70. Wakati huo Yosefu alikuwa amekwisha tangulia kukaa huko Misri. Baadaye, Yosefu alifariki, hali kadhalika ndugu zake na kizazi kile chote. Lakini wazawa wa Israeli waliongezeka sana, wakawa wengi na wenye nguvu mno, wakaenea kila mahali nchini Misri. Basi, akatokea mfalme mwingine huko Misri ambaye hakumjua Yosefu. Naye akawaambia watu wake, “Tazameni jinsi Waisraeli walivyo wengi na wenye nguvu kuliko sisi. Ni lazima tutafute hila ya kuwapunguza na kuzuia wasiongezeke; la sivyo, kama vita vikitokea watajiunga na adui zetu na kuitoroka nchi.” Basi, Wamisri wakawateua wanyapara wawasimamie Waisraeli na kuwatesa kwa kazi ngumu. Waisraeli wakafanya kazi ya kumjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kadiri walivyoteswa ndivyo Waisraeli walivyozidi kuongezeka na kuenea nchini. Hivyo Wamisri wakawaogopa sana watu wa Israeli. Basi, Wamisri wakawatumikisha Waisraeli kikatili, wakayafanya maisha yao kuwa magumu kwa kazi ngumu ya kutengeneza chokaa na kufyatua matofali, na kazi zote za shambani. Katika kazi hizo zote, Waisraeli walitumikishwa kwa ukatili. Kisha, mfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Misri, Shifra na Pua, ambao waliwahudumia wanawake wa Kiebrania, “Mnapowahudumia wanawake wa Kiebrania wanapojifungua, ikiwa mtoto anayezaliwa ni wa kiume, muueni. Lakini ikiwa ni wa kike, mwacheni aishi.” Lakini kwa kuwa wakunga hao walimcha Mungu, hawakufanya kama walivyoamriwa na mfalme wa Misri, bali waliwaacha watoto wa kiume wa Waisraeli waishi. Basi, mfalme wa Misri akawaita wakunga hao, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivyo? Mbona mmewaacha watoto wa kiume waishi?” Wao wakamjibu Farao, “Wanawake wa Kiebrania si sawa na wanawake wa Misri. Wao ni hodari; kabla mkunga hajafika, wao huwa wamekwisha jifungua.” Basi, Mungu akawajalia mema wakunga hao, nao Waisraeli wakazidi kuongezeka na kuwa na nguvu sana. Na kwa vile wakunga hao walimcha Mungu, Mungu akawajalia kupata jamaa zao wenyewe. Kisha Farao akawaamuru watu wake wote hivi, “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania mtupeni mtoni Nili. Lakini kila mtoto wa kike, mwacheni aishi.” Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa Walawi aliyemwoa mwanamke mmoja ambaye pia alikuwa wa ukoo wa Walawi. Basi, mama huyu akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Alipoona kwamba mtoto huyo mchanga alikuwa mzuri, akamficha kwa muda wa miezi mitatu. Lakini kwa vile hakuweza kumficha zaidi ya muda huo, alitengeneza namna ya kikapu cha mafunjo, akakipaka namna ya lami, akamtia huyo mtoto ndani. Kisha akakiweka kikapu kando ya mto Nili kwenye majani. Dada yake huyo mtoto akajificha karibu na mahali hapo ili aone yatakayompata nduguye. Basi, binti Farao akashuka mtoni kuoga, na watumishi wake wakawa wanatembeatembea kandokando ya mto. Binti Farao akakiona kile kikapu katika majani, akamtuma mjakazi wake akichukue. Alipokifungua, alimwona yule mtoto mchanga, analia. Basi, akamwonea huruma, akasema, “Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.” Papo hapo dada yake yule mtoto akajitokeza, akamwambia binti Farao, “Je, niende nikakutafutie yaya miongoni mwa wanawake wa Kiebrania akulelee mtoto huyu?” Binti Farao akamwambia, “Naam; nenda.” Basi, huyo msichana akaenda, akamwita mama yake huyo mtoto. Binti Farao akamwambia huyo mama, “Mtunze mtoto huyu, umlee kwa niaba yangu, nami nitakulipa mshahara wako.” Basi, huyo mama akamchukua mtoto, akamlea. Mtoto alipokuwa mkubwa kiasi, mama yake akampeleka kwa binti Farao, naye akamchukua na kumfanya mwanawe. Binti Farao akasema, “Nimemtoa majini,” kwa hiyo akampa mtoto huyo jina Mose. Siku moja, Mose alipokuwa mtu mzima, aliwaendea Waebrania wenzake ili kujionea taabu zao. Basi, akamwona Mmisri mmoja anampiga Mwebrania, mmoja wa ndugu zake Mose. Mose akatazama huku na huko, na alipoona kwamba hakuna mtu karibu, alimuua yule Mmisri na kumficha mchangani. Kesho yake, Mose alitoka tena, akaona Waebrania wawili wanapigana. Basi, akamwuliza yule aliyekosea, “Kwa nini unampiga mwenzako?” Naye akamjibu, “Nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Hivyo, Mose aliogopa na kufikiri, “Bila shaka jambo hilo limejulikana!” Naye Farao aliposikia juu ya tukio hilo akakusudia kumuua Mose. Lakini Mose alimkimbia Farao, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani. Siku moja, Mose alikuwa ameketi kando ya kisima cha maji. Basi, binti saba wa kuhani mmoja wa huko Midiani walifika kuchota maji na kuwanywesha kondoo na mbuzi wa baba yao. Wachungaji wengine wakaja na kuwafukuza hao binti. Lakini Mose akawasaidia binti hao na kuwanywesha wanyama wao. Walipomrudia baba yao Reueli, yeye akawauliza, “Mbona leo mmerudi upesi hivyo?” Nao wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa mikononi mwa wale wachungaji, naye mwenyewe akachota maji na kuwanywesha wanyama wetu.” Baba yao akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha huko? Mwiteni aje ale chakula.” Mose akakubali kukaa kwa huyo mtu. Basi, huyo mtu akampa Mose binti yake aitwaye Zipora awe mke wake. Zipora akamzalia mtoto wa kiume. Mose akasema, “Nimekimbilia katika nchi ya kigeni”, kwa hiyo akampa huyo mtoto jina Gershomu. Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakapiga kite na kulia kutokana na hali yao ya utumwa, na kilio chao kikamfikia Mungu juu. Mungu akasikia kilio chao, naye akakumbuka agano alilofanya na Abrahamu, na Isaka na Yakobo. Mungu aliwaangalia Waisraeli, akaona kuwa hali yao ni mbaya. Siku moja, Mose alikuwa anachunga kundi la kondoo la baba mkwe wake, Yethro, kuhani wa Midiani. Mose alilipeleka kundi hilo upande wa magharibi wa jangwa, akaufikia mlima Horebu, mlima wa Mungu. Basi, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea katika mwali wa moto katikati ya kichaka. Mose akaangalia, akashangaa kuona kichaka kinawaka moto na wala hakiungui. Basi, akajisemea, “Hiki ni kioja! Kichaka kuwaka moto na kisiungue? Hebu nitazame vizuri.” Mwenyezi-Mungu alipoona kwamba Mose amegeuka kukiangalia kichaka, akamwita pale kichakani, “Mose! Mose!” Mose akaitika, “Naam! Nasikiliza!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Usije karibu! Vua viatu vyako kwa sababu mahali unaposimama ni mahali patakatifu.” Kisha Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako; Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo.” Mose akaufunika uso wake kwa kuwa aliogopa kumwangalia Mungu. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nimeyaona mateso ya watu wangu walioko nchini Misri na nimekisikia kilio chao kinachosababishwa na wanyapara wao. Najua mateso yao, na hivyo, nimeshuka ili niwaokoe mikononi mwa Wamisri. Nitawatoa humo nchini na kuwapeleka katika nchi nzuri na kubwa; nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Naam, kilio cha Waisraeli kimenifikia; nimeona jinsi Wamisri wanavyowatesa. Sasa, nitakutuma kwa Farao ili uwatoe watu wangu, watu hao wa Israeli, kutoka nchini Misri.” Lakini Mose akamwambia Mungu, “Mimi ni nani hata nimwendee Farao na kuwatoa Waisraeli nchini Misri?” Mungu akamwambia, “Mimi nitakuwa pamoja nawe. Utawatoa watu wa Israeli na kuja kuniabudu mimi Mungu juu ya mlima huu. Hiyo itakuwa ishara kwamba ni mimi Mungu niliyekutuma wewe.” Hapo, Mose akamwambia Mungu, “Sasa, nikiwaendea Waisraeli na kuwaambia, ‘Mungu wa babu zenu amenituma kwenu,’ nao wakiniuliza, ‘Jina lake ni nani,’ nitawaambia nini?” Mungu akamjibu, “MIMI NDIMI NILIYE. Waambie hivi watu wa Israeli: Yule anayeitwa, NDIMI NILIYE, amenituma kwenu. Waambie hivi Waisraeli: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu. Hili ndilo jina langu milele, na hivyo ndivyo nitakavyokumbukwa katika vizazi vyote. Nenda ukawakusanye wazee wa Israeli na kuwaambia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu: Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea na kusema, ‘Nimewachunguzeni na kuyaona mambo mnayotendewa nchini Misri! Naahidi kuwa nitawatoa katika mateso yenu huko Misri na kuwapeleka katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi; nitawapeleka katika nchi inayotiririka maziwa na asali.’ “Wao watakusikiliza, nawe pamoja na wazee wa Waisraeli mtamwendea mfalme wa Misri na kumwambia, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, ametutokea. Sasa, uturuhusu tuende safari ya mwendo wa siku tatu jangwani, tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’ Najua kuwa mfalme wa Misri hatawaacha mwende asipolazimishwa kwa mkono wenye nguvu. Kwa hiyo nitaunyosha mkono wangu na kuipiga nchi ya Misri kwa maajabu ambayo nitayafanya huko. Baadaye mfalme atawaacha mwondoke. Tena nitahakikisha Wamisri wanawapendelea Waisraeli, na mtakapoondoka Misri, hamtatoka mikono mitupu. Kila mwanamke Mwebrania atamwomba jirani yake Mmisri, au mgeni wake aliye nyumbani kwake, ampe vito vya fedha na dhahabu pamoja na nguo. Hivyo mtawavisha watoto wenu wa kiume na wa kike. Ndivyo mtakavyowapokonya Wamisri mali yao.” Mose akamwambia Mungu, “Lakini Waisraeli hawataniamini wala kunisikiliza, bali watasema kuwa wewe Mwenyezi-Mungu hukunitokea.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Unashika nini mkononi mwako?” Mose akamwambia, “Fimbo.” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Itupe chini.” Mose akaitupa fimbo chini, nayo ikageuka kuwa nyoka! Mose akaikimbia. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako, umkamate mkia!” Mose akanyosha mkono wake, akamkamata; nyoka akageuka tena kuwa fimbo mkononi mwake. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Hivyo Waisraeli watapata kuamini kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo, nimekutokea.” Tena, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Ingiza mkono wako kifuani mwako.” Mose akafanya hivyo, lakini alipoutoa nje, kumbe ukawa na ukoma; mweupe kama theluji. Kisha Mungu akamwambia, “Ingiza tena mkono wako kifuani mwako!” Mose akauingiza mkono wake kifuani. Na alipoutoa nje, kumbe ukarudia hali yake ya kawaida kama ulivyo mwili wake. Mungu akamwambia Mose, “Wasipokuamini au kusadiki ishara ya kwanza, yawezekana wakaamini ishara ya pili. Lakini wasipoamini hata ishara hizi mbili, au kuamini maneno yako, utachota maji ya mto Nili na kuyamwaga juu ya nchi kavu. Maji hayo yatakuwa damu juu ya nchi kavu.” Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Ewe Bwana wangu, mimi sina ufasaha wa kuongea tangu zamani; hata baada ya wewe kusema nami mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Ni nani aliyeumba kinywa cha mtu? Ni nani amfanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi? Aone au awe kipofu? Je, si mimi Mwenyezi-Mungu? Basi, nenda! Mimi nitakiongoza kinywa chako na kukufundisha cha kusema.” Lakini Mose akasema, “Ee Bwana wangu, tafadhali nakusihi, umtume mtu mwingine.” Ndipo hasira ya Mungu ilipowaka dhidi ya Mose, akamwambia, “Je, si yuko ndugu yako Aroni ambaye ni Mlawi? Najua yeye ana ufasaha wa kuongea. Tena anakuja kukutana nawe, na mara tu atakapokuona atafurahi moyoni. Wewe utaongea naye na kumwambia yote atakayosema. Mimi nitawasaidieni na kuwafundisha mambo mtakayofanya. Aroni ataongea na Waisraeli kwa niaba yako. Yeye atakuwa msemaji wako, nawe utakuwa kama Mungu kwake. Utaichukua mkononi mwako fimbo hii ambayo utaitumia kufanya zile ishara.” Mose alirudi kwa Yethro, baba mkwe wake, akamwambia, “Tafadhali niruhusu nirudi Misri kwa ndugu zangu, nikaone kama bado wako hai.” Yethro akamwambia, “Nenda kwa amani.” Mose akiwa bado nchini Midiani, Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi Misri kwa sababu wale wote waliotaka kukuua wamekwisha kufa.” Basi, Mose akamchukua mkewe na watoto wake, akawapandisha juu ya punda, akaanza safari ya kurudi Misri. Mkononi mwake alichukua ile fimbo aliyoamriwa na Mungu aichukue. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utakapofika Misri, hakikisha kwamba umetenda mbele ya Farao miujiza yote niliyokupa uwezo kuifanya. Lakini mimi nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hatawaachia Waisraeli waondoke. Nawe utamwambia Farao kuwa Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Israeli ni mzaliwa wangu wa kwanza wa kiume! Nami nakuambia: Mwache mwanangu aondoke, ili anitumikie! Kama ukikataa kumwachia aondoke, tazama nitamuua mzaliwa wako wa kwanza wa kiume.’” Akiwa bado njiani kurudi Misri, Mose alikuwa mahali pa kulala wageni; basi, Mungu alikutana naye na kutaka kumuua. Hapo Zipora akakimbia haraka, akachukua jiwe kali, akalikata govi la mwanawe na kumgusa nalo Mose miguuni akisema, “Wewe ni bwana harusi wa damu”. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwacha Mose. Zipora alikuwa amesema, “Bwana harusi wa damu,” kwa sababu ya kutahiri. Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Nenda jangwani ukakutane na Mose.” Basi, Aroni akaenda, akakutana na Mose kwenye mlima wa Mungu, akambusu. Naye Mose akamwambia Aroni maneno yote aliyoambiwa na Mwenyezi-Mungu ayaseme, na miujiza yote aliyoagizwa atende. Kisha Mose na Aroni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli. Aroni akawaambia maneno yote Mwenyezi-Mungu aliyokuwa amemwagiza Mose, na kuifanya ile miujiza mbele ya watu wote. Watu wakaamini. Na waliposikia kwamba Mwenyezi-Mungu amewajia kuwasaidia Waisraeli, na kwamba ameyaona mateso yao, wote wakainamisha vichwa vyao na kumwabudu. Baadaye, Mose na Aroni walimwendea Farao, wakamwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli anasema hivi, ‘Waache watu wangu waondoke, wakanifanyie sikukuu jangwani.’” Lakini Farao akawauliza, “Ni nani huyo Mwenyezi-Mungu, hata nimsikilize na kuwaacha Waisraeli waondoke? Mimi simtambui huyo Mwenyezi-Mungu, wala sitawaruhusu Waisraeli waondoke.” Mose na Aroni wakamwambia, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Tunakusihi utuache twende zetu jangwani mwendo wa siku tatu tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. La sivyo, yeye atatuua kwa maradhi mabaya au vita.” Lakini mfalme wa Misri akawajibu, “Enyi Mose na Aroni, kwa nini mnajaribu kuwatoa watu kazini mwao? Rudini kazini mwenu.” Tena Farao akasema, “Hawa watu wenu ni wengi kuliko wananchi; mnataka waache kufanya kazi!” Siku hiyohiyo Farao aliwaamuru wanyapara pamoja na wasimamizi, akasema, “Tangu leo msiwape watu hawa nyasi za kutengenezea matofali kama ilivyo kawaida. Wao wenyewe watakwenda kujitafutia. Lakini idadi ya matofali yanayotengenezwa kila siku iwe ileile, wala lisipungue hata tofali moja, kwa kuwa watu hawa ni wavivu ndio maana wanapiga kelele: ‘Tuache twende tukamtambikie Mungu wetu.’ Wazidishieni watu hawa kazi ngumu ili waitolee jasho na kuacha kusema maneno ya uongo.” Basi, wanyapara na wasimamizi wa watu wakatoka na kuwaambia watu, “Farao anasema hivi, ‘Sitawapeni nyasi. Nendeni nyinyi wenyewe mkatafute popote mtakapoweza kuzipata, na wala kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’” Basi, watu wote wakatawanyika kila mahali nchini Misri wakitafuta nyasi za kutengenezea matofali. Nao Wanyapara wakakazana wakisema, “Timizeni kazi yenu ya kila siku kama hapo awali mlipoletewa nyasi.” Wanyapara Wamisri wakawapiga wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa kusimamia kazi wakisema, “Kwa nini hamtimizi kazi yenu na kufikisha idadi ileile ya matofali kama awali?” Ndipo wasimamizi wa Waisraeli walipomwendea Farao, wakamlilia wakisema, “Kwa nini unatutenda hivi sisi watumishi wako? Hatupewi tena nyasi zozote na huku tunalazimishwa kufyatua matofali. Tena sisi watumishi wako tunapigwa, hali kosa ni la watu wako.” Lakini Farao akasema, “Wavivu nyinyi; nyinyi ni wavivu, ndio maana mnasema, ‘Tuache twende tukamtambikie Mwenyezi-Mungu’. Nendeni sasa mkafanye kazi; maana hamtapewa nyasi zozote na mtafyatua idadi ileile ya matofali.” Basi, hao wasimamizi wa Waisraeli sasa walijiona kuwa wako taabuni, kwani waliambiwa, “Hamtaipunguza kamwe idadi ya matofali ya kila siku.” Walipoondoka kwa Farao, walikutana na Mose na Aroni ambao walikuwa wanawangojea. Basi, wakawaambia Mose na Aroni, “Mwenyezi-Mungu na aone jambo hili na kuwahukumu nyinyi kwa sababu mmetufanya sisi kuwa chukizo kwa Farao na maofisa wake; nyinyi mmewapa sababu ya kutuua.” Kisha Mose akamgeukia tena Mwenyezi-Mungu, akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, kwa nini unawatendea watu hawa uovu? Kwa nini hata ulinituma? Tangu nilipokwenda na kuongea na Farao kwa jina lako, yeye amewatendea uovu watu hawa. Wewe hujafanya lolote kuwakomboa watu wako.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu Mose, “Sasa utaona jinsi nitakavyomtenda Farao; maana kwa nguvu atalazimika kuwaacha watu wangu watoke. Naam, kwa nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.” Mungu akamwambia Mose, “Mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nilimtokea Abrahamu, Isaka na Yakobo nikijulikana kama Mungu Mwenye Nguvu, ingawa kwa jina langu, Mwenyezi-Mungu, sikuwajulisha. Tena nilifanya agano nao kwamba nitawapa nchi ya Kanaani ambako waliishi kama wageni. Zaidi ya hayo, nimesikia kilio cha Waisraeli ambao wamelazimishwa kufanya kazi za kitumwa na Wamisri, nikalikumbuka agano langu. Kwa hiyo, waambie Waisraeli hivi, ‘Mimi ni Mwenyezi-Mungu! Mimi nitawatoa katika nira mlizowekewa na Wamisri. Nitawaokoeni utumwani mwenu. Nitaunyosha mkono wangu wenye nguvu na kuwaadhibu vikali Wamisri na kuwakomboa nyinyi. Nitawafanyeni kuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Nyinyi mtatambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa katika nira za Wamisri. Nami nitawapeleka katika nchi ile niliyoapa kumpa Abrahamu, Isaka na Yakobo. Nitawapeni nchi hiyo iwe yenu. Mimi ni Mwenyezi-Mungu.’” Mose akawaeleza Waisraeli maneno hayo. Lakini wao hawakumsikiliza kwa sababu walikuwa wamekufa moyo kutokana na utumwa mkali. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao, mfalme wa Misri, umwambie awaache Waisraeli waondoke nchini mwake.” Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama, Waisraeli hawanisikilizi mimi, sembuse Farao! Tena mimi ni mtu asiye na ufasaha wa kuongea!” Lakini Mwenyezi-Mungu akaongea na Mose na Aroni, akawaagiza waende kwa Farao, mfalme wa Misri, na kuwatoa Waisraeli nchini Misri. Hii ndiyo orodha ya wakuu wa jamaa za Waisraeli, Wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli: Henoki, Palu, Hesroni na Karmi. Hao walikuwa mababu wa jamaa za Reubeni. Wana wa Simeoni walikuwa: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli; huyu wa mwisho alikuwa mtoto wa mwanamke wa Kikanaani. Hao walikuwa mababu wa jamaa za Simeoni. Sasa yafuata majina ya wana wa Lawi na wazawa wao: Gershoni, Kohathi na Merari. Lawi aliishi miaka 137. Wana wa Gershoni walikuwa: Libni na Shimei; jamaa zao zilitajwa kwa majina yao. Wana wa Kohathi walikuwa: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli. Kohathi aliishi miaka 133. Wana wa Merari walikuwa: Mahli na Mushi. Hao ndio mababu wa jamaa za Walawi. Amramu alimwoa Yokebedi, shangazi yake, naye akamzalia Aroni na Mose. Amramu aliishi miaka 137. Na watoto wa kiume wa Ishari walikuwa: Kora, Nefegi na Zikri. Watoto wa kiume wa Uzieli walikuwa: Mishaeli, Elsafani na Sithri. Aroni alimwoa Elisheba, binti yake Aminadabu, dada yake Nashoni; naye akamzalia Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari. Nao watoto wa kiume wa Kora walikuwa: Asiri, Elkana na Abiasafu, ambao walikuwa mababu wa jamaa za Kora. Eleazari, mwana wa Aroni, alimwoa mmoja wa binti za Putieli, naye akamzalia Finehasi. Hawa ndio waliokuwa wakuu wa jamaa za Lawi. Aroni na Mose ndio walioambiwa na Mwenyezi-Mungu, “Watoeni watu wa Israeli kutoka nchi ya Misri, vikundi kwa vikundi.” Ndio haohao Mose na Aroni walioongea na Farao, mfalme wa Misri, juu ya kuwatoa Waisraeli nchini Misri. Siku ile Mwenyezi-Mungu alipoongea na Mose nchini Misri, alimwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. Mwambie Farao, mfalme wa Misri, maneno yote ninayokuambia.” Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Mimi sina ufasaha wa kuongea; Farao atanisikilizaje?” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tazama, mimi nakufanya kuwa kama mungu kwa Farao, naye ndugu yako Aroni atakuwa nabii wako. Utamwambia ndugu yako Aroni mambo yote nitakayokujulisha, naye Aroni nduguyo, atamwambia Farao awaache Waisraeli watoke nchini mwake. Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Na hata kama nitazidisha miujiza na maajabu yangu katika nchi ya Misri, Farao hatakusikiliza, na hapo nitaunyosha mkono wangu wenye nguvu na kuiadhibu vikali nchi ya Misri, na kuwatoa watu wangu, makabila ya Israeli, kutoka Misri. Nitafanya hivyo kwa matendo makuu ya hukumu dhidi ya Misri. Wakati nitakapounyosha mkono wangu dhidi ya nchi ya Misri na kuwatoa Waisraeli miongoni mwao. Ndipo Wamisri watakapotambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mose na Aroni wakafanya hivyo; naam, walifanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Mose alikuwa na umri wa miaka themanini, na Aroni alikuwa na umri wa miaka themanini na mitatu wakati huo walipoongea na Farao. Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Farao atakapowaambieni mthibitishe jambo hilo kwa kutenda miujiza, wewe utamwambia Aroni aichukue fimbo yake, aitupe mbele ya Farao, nayo itakuwa nyoka.” Basi, Mose na Aroni wakamwendea Farao na kufanya kama walivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Aroni aliitupa fimbo yake chini mbele ya Farao na maofisa wake, nayo ikawa nyoka. Lakini, Farao akawaita wenye hekima wake na wachawi; hao wachawi wa Misri wakafanya vivyo hivyo kwa uchawi wao. Kila mmoja akaitupa fimbo yake chini, ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza fimbo zao. Hata hivyo, moyo wa Farao bado ulibaki kuwa mgumu, wala hakuwasikiliza; ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Moyo wa Farao umekuwa mgumu. Anakataa kuwaacha Waisraeli waondoke. Basi, nenda ukakutane naye kesho asubuhi, wakati anapokwenda mtoni Nili. Mngojee kando ya mto. Chukua mkononi mwako ile fimbo iliyogeuka kuwa nyoka. Kisha mwambie hivi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, amenituma kwako, naye asema hivi, ‘Waache watu wangu waende zao ili wanitumikie jangwani, lakini mpaka sasa wewe hupendi kutii. Basi, Mwenyezi-Mungu asema kwamba sasa utamtambua yeye ni nani. Nitayapiga maji ya mto Nili kwa fimbo hii, na maji yote yatageuka kuwa damu. Samaki waliomo mtoni Nili watakufa, mto wote utanuka vibaya, na Wamisri watachukia kabisa kunywa maji yake.’” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni aichukue fimbo yake na kuinyosha juu ya maji ya Misri, juu ya mito yote, mifereji, madimbwi na mabwawa yao yote, nayo yatakuwa damu. Kutakuwa na damu nchini kote, na hata katika vyombo vyote vya mbao na vya mawe.” Mose na Aroni wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Aroni aliinua fimbo yake juu mbele ya Farao na maofisa wake, akayapiga maji ya mto Nili, na maji yote mtoni yakageuka kuwa damu. Samaki wakafa, mto ukanuka vibaya sana hata Wamisri wasiweze kunywa maji yake. Nchi nzima ikajaa damu. Lakini wachawi wa Misri kwa kutumia uchawi wao wakafanya vivyo hivyo. Kwa hiyo moyo wa Farao ukabaki kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni; ikawa kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema. Basi, Farao akarudi nyumbani kwake, na hata haya yaliyotokea hakuyajali. Wamisri wote wakachimbachimba kandokando ya mto Nili ili wapate maji ya kunywa, kwani hawakuweza kunywa maji ya mto huo. Pigo hilo la mto Nili lilidumu siku saba. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie Mwenyezi-Mungu asema hivi: Waache watu wangu waondoke ili wanitumikie. Lakini ukikataa kuwaacha waondoke, basi, nitaipiga nchi yako yote kwa kuiletea vyura. Mto Nili utafurika vyura, nao wataingia mpaka ndani ya nyumba yako, chumba chako cha kulala, kitandani mwako, na katika nyumba za watumishi wako na watu wako. Vyura hao wataingia katika majiko yenu na vyombo vyenu vya kukandia unga. Vyura watapanda juu ya mwili wako, miili ya watu wako na watumishi wenu!” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni anyoshe mkono wake na fimbo yake juu ya mito, juu ya mifereji na madimbwi, nao vyura watatokea na kuenea kila mahali nchini Misri.” Basi, Aroni akanyosha fimbo yake juu ya maji yote, vyura wakatokea na kuifunika nchi nzima ya Misri. Lakini wachawi wa Misri kwa uchawi wao pia wakaleta vyura nchini Misri. Kisha Farao akamwita Mose na Aroni, akamwambia, “Msihi Mwenyezi-Mungu, ili aniondolee mimi na watu wangu vyura hawa, nami nitawaacha Waisraeli waende zao na kumtambikia Mwenyezi-Mungu.” Mose akamjibu Farao, “Haya! Waweza kutaja wakati unaotaka nikuombee kwa Mungu, niwaombee maofisa wako na watu wako; nitamwomba awaangamize vyura hawa waliomo katika nyumba zenu; watabaki tu mtoni Nili!” Farao akamwambia, “Kesho.” Mose akasema, “Nitafanya kama unavyosema, ili ujue kwamba hakuna yeyote anayelingana na Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Vyura wataondoka kwako, na kwenye nyumba zenu, kwa maofisa wako na kwa watu wako; watabaki tu katika mto Nili.” Basi, Mose na Aroni wakaondoka nyumbani kwa Farao, na Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu amwondolee Farao uvamizi wa vyura hao aliomletea. Mwenyezi-Mungu akafanya kama Mose alivyomwomba: Vyura wakafa majumbani, viwanjani na kwenye kumbi za nyumba na katika mashamba. Watu wakawakusanya vyura hao marundo marundo; nchi nzima ikanuka. Lakini Farao alipoona kwamba nchi imepata nafuu, akawa mkaidi tena, wala hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni anyoshe fimbo yake na kuyapiga mavumbi, nayo yatageuka kuwa viroboto kote nchini Misri.” Mose na Aroni wakafanya hivyo. Aroni alinyosha fimbo yake na kuyapiga mavumbi, nayo yakageuka kuwa viroboto na kuwaparamia watu na wanyama. Mavumbi yote nchini kote Misri yakageuka kuwa viroboto. Wachawi wa Misri, kwa uchawi wao, wakajaribu kuyageuza mavumbi yawe viroboto, lakini hawakufaulu. Viroboto hao wakaenea juu ya watu na wanyama. Wale wachawi wakamwambia Farao, “Hii ni kazi ya mkono wa Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukaendelea kuwa mgumu; wala hakuwasikiliza Mose na Aroni. Ikawa kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kesho amka asubuhi mapema umwendee Farao wakati anapokwenda mtoni umwambie, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Waache watu wangu waondoke ili wanitumikie. Kama ukikataa kuwaacha waondoke, basi, nitakuletea makundi ya nzi, wewe, maofisa wako na watu wako wote. Wataingia kwenye nyumba zenu na nyumba zote za Wamisri zitajaa makundi ya nzi, kadhalika na ardhi yote ya Misri. Lakini siku hiyo sehemu ya Gosheni wanakoishi watu wangu nitaikinga: Humo nzi hao hawatakuwamo. Hapo ndipo utakapotambua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu natenda mambo nchini mwako. Nitawakinga watu wangu na mambo yatakayowapata watu wako. Mambo hayo yatafanyika kesho.’” Mwenyezi-Mungu akafanya kama alivyosema: Makundi makubwa ya nzi yakaivamia nyumba ya Farao, nyumba za maofisa wake na nchi nzima ya Misri. Nchi nzima ya Misri ikaharibiwa na nzi hao. Ndipo Farao akawaita Mose na Aroni, akasema, “Mnaweza kwenda kumtambikia Mungu wenu, lakini iwe humuhumu nchini Misri.” Lakini Mose akamjibu, “La! Haifai kufanya hivyo, maana tambiko tutakazomtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, zitawachukiza Wamisri. Je, Wamisri wakituona tukitoa tambiko ambazo ni chukizo kwao, si watatupiga mawe? Ni lazima tusafiri mwendo wa siku tatu jangwani tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama atakavyotuamuru.” Basi, Farao akasema, “Nitawaacha mwende zenu kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, jangwani. Walakini msiende mbali mno. Niombeeni na mimi.” Mose akamjibu, “Mara tu nitakapokuacha, nitamwomba Mwenyezi-Mungu makundi haya ya nzi yatoweke kwako wewe Farao, maofisa wako na watu wako, kesho. Lakini wewe usitudanganye tena kwa kukataa kuwaacha watu kwenda kumtambikia Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mose akaondoka nyumbani kwa Farao, akamwomba Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akafanya kama Mose alivyomwomba, wale nzi wakatoweka kutoka kwa Farao, maofisa wake na watu wake, wala hakusalia hata mmoja. Lakini hata safari hii Farao alikuwa mkaidi, wala hakuwaruhusu Waisraeli kuondoka. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, nasema, ‘Waache watu wangu waondoke ili wakanitumikie. Kama ukikataa kuwaacha waondoke na ukiendelea kuwashikilia, nitaunyosha mkono wangu na kuleta maradhi mabaya sana juu ya mifugo yenu yote: Ng'ombe, farasi, punda, ngamia, mbuzi na kondoo. Na, nitaitenganisha mifugo ya Waisraeli na mifugo ya Wamisri ili mnyama hata mmoja wa Waisraeli asife.’” Tena, Mwenyezi-Mungu akaweka wakati maalumu akisema, “Kesho mimi Mwenyezi-Mungu nitatekeleza jambo hilo nchini Misri.” Kesho yake Mwenyezi-Mungu akafanya alichosema. Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna mnyama hata mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Farao akauliza habari juu ya wanyama wa Waisraeli, akaambiwa kuwa hakuna mnyama wao hata mmoja aliyekufa. Hata hivyo, Farao akabaki mkaidi, wala hakuwaruhusu Waisraeli waondoke. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Chukueni kila mmoja wenu magao ya majivu ya tanuri, kisha Mose ayarushe juu hewani mbele ya Farao. Majivu hayo yatakuwa vumbi nyembamba itakayoenea juu ya nchi yote ya Misri. Yatasababisha majipu yatakayotumbuka na kuwa vidonda kwa watu na wanyama kila mahali nchini Misri.” Basi, wakachukua majivu kutoka kwenye tanuri, wakamwendea Farao, naye Mose akayarusha juu hewani. Watu na wanyama wakavamiwa na majipu hata wale wachawi hawakuweza kujitokeza maana wao pamoja na Wamisri wote pia walivamiwa na majipu hayo. Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, naye hakuwasikiliza kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kesho, amka alfajiri na mapema umwendee Farao, umwambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, nasema hivi, ‘Waache watu wangu waondoke ili wakanitumikie. Maana safari hii, wewe mwenyewe, maofisa wako na watu wako mtakumbana na mapigo yangu makali. Nawe utatambua kwamba hakuna yeyote duniani aliye kama mimi. Ningalikwisha kukuangamiza tayari wewe na watu wako kwa maradhi mabaya, nanyi mngalikuwa mmekwisha angamia. Lakini nimewaacheni muishi ili kudhihirisha uwezo wangu. Kwa hiyo dunia yote itatambua kuwa mimi ni nani. Lakini bado unaonesha kiburi dhidi ya watu wangu, wala huwaachi waondoke. Kwa hiyo kesho, wakati kama huu, nitaleta mvua kubwa ya mawe ambayo haijawahi kutokea nchini Misri, tangu mwanzo wake hadi leo. Kwa hiyo agiza mifugo yako na chochote kilicho huko mashambani viwekwe mahali salama; kwa maana mvua ya mawe itamnyeshea kila mtu na mnyama aliye shambani na ambaye hayuko nyumbani; wote watakufa.’” Baadhi ya maofisa wa Farao waliyatia maanani maneno hayo ya Mwenyezi-Mungu, wakawapeleka watumwa na wanyama wao nyumbani mahali pa usalama. Lakini yule ambaye hakulijali neno la Mwenyezi-Mungu aliwaacha watumwa wake na wanyama wake mashambani. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu mbinguni, ili mvua ya mawe inyeshe kila mahali nchini Misri. Imnyeshee mtu, mnyama na kila mmea shambani.” Basi, Mose alinyosha fimbo yake kuelekea mbinguni. Naye Mwenyezi-Mungu akaleta mvua ya mawe na ngurumo; umeme ukaipiga nchi. Mwenyezi-Mungu alinyesha mvua ya mawe nchini Misri, mvua kubwa ya mawe iliyoandamana na mfululizo wa umeme, ambayo hakuna mwananchi yeyote wa Misri aliyepata kamwe kushuhudia kabla. Mvua hiyo ya mawe ilivunjavunja kila kitu katika mashamba na kila mahali nchini Misri: Wanyama na watu. Mawe ya mvua yakavunjavunja mimea yote na miti mashambani. Jambo hilo lilifanyika kote nchini Misri isipokuwa tu sehemu ya Gosheni walimokaa Waisraeli; humo haikuwako mvua ya mawe. Basi, Farao akaagiza Mose na Aroni waitwe, akawaambia, “Safari hii nimetenda dhambi. Mwenyezi-Mungu ana haki; mimi na watu wangu tumekosa. Mwombeni Mwenyezi-Mungu kwani ngurumo hii na mvua ya mawe vimezidi. Mimi nitawaacheni mwondoke na wala hamtakaa tena zaidi.” Mose akamwambia, “Mara tu nitakapotoka nje ya mji nitainua mikono na kumwomba Mwenyezi-Mungu. Ngurumo itakoma na hakutakuwa na mvua ya mawe tena ili utambue kwamba dunia ni yake Mwenyezi-Mungu. Lakini najua kwamba wewe na maofisa wako bado hammwogopi Mwenyezi-Mungu.” (Kitani na mimea ya shayiri vyote vilikuwa vimeharibiwa, kwa sababu shayiri ilikuwa na masuke, na kitani ilikuwa imechanua maua. Lakini ngano na jamii nyingine ya ngano havikuharibiwa kwa kuwa hiyo huchelewa kukomaa). Basi, Mose akaondoka nyumbani kwa Farao, akatoka nje ya mji. Kisha akainua mikono yake kumwomba Mwenyezi-Mungu. Ngurumo na mvua ya mawe vikakoma; mvua ikaacha kunyesha duniani. Lakini Farao alipoona kuwa mvua ya mawe na ngurumo vimekoma, aliirudia dhambi yake tena, akawa mkaidi, yeye pamoja na maofisa wake. Basi, kama Mwenyezi-Mungu alivyombashiria Mose, Farao alikaidi akakataa kuwaruhusu Waisraeli waondoke. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao. Mimi nimemfanya kuwa mkaidi na maofisa wake ili nipate kutenda ishara hizi miongoni mwao, ili nyinyi mpate kuwasimulia watoto wenu na wajukuu wenu, jinsi nilivyowadhihaki Wamisri kwa kuzifanya ishara hizo miongoni mwao. Hivyo mtatambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mose na Aroni wakamwendea Farao na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, anasema hivi, ‘Mpaka lini utakataa kujinyenyekesha mbele yangu? Waache watu wangu waondoke ili wapate kunitumikia. Ukikataa kuwaacha watu wangu waondoke, basi, kesho nitaleta nzige waivamie nchi yako. Nchi yote ya Misri itakuwa giza kwa sababu ya nzige hao. Watakula kila kitu kilichosalimika baada ya ile mvua ya mawe; pia hawataacha chochote juu ya miti inayoota mashambani. Nzige hao watajaa katika nyumba zako, nyumba za maofisa wako na za Wamisri wote; watakuwa wengi kiasi ambacho hata wazee wenu hawajapata kuona tangu walipozaliwa, hadi leo.’” Basi, Mose akatoka kwa Farao. Viongozi wa Farao wakamwuliza, “Je, mtu huyu atatusumbua mpaka lini? Waache watu hawa waende zao wakamtumikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Je, hujali kwamba nchi ya Misri inaangamia?” Hapo, Mose na Aroni wakaitwa warudi kwa Farao, naye akawaambia, “Nendeni mkamtumikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Lakini, nauliza: Ni kina nani watakaokwenda pamoja nanyi?” Mose akamjibu, “Kila mtu: Vijana na wazee, tutaondoka na watoto wetu wa kiume na wa kike, kondoo na mbuzi wetu na ng'ombe; kwa maana ni lazima tumfanyie sikukuu Mwenyezi-Mungu.” Kwa kuwapuuza, Farao akawaambia, “Ehe! Mwenyezi-Mungu awe nanyi kama nitawaruhusu kamwe mwende zenu na watoto wenu. Ni dhahiri kwamba mnayo nia mbaya moyoni mwenu. La hasha! Ni wanaume tu watakaokwenda kumtumikia Mwenyezi-Mungu, maana hilo ndilo mnalotaka.” Hapo Mose na Aroni wakafukuzwa mbele ya Farao. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri, nzige watokee ili waingie na kula mimea yote nchini na vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe.” Basi, Mose akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri. Mwenyezi-Mungu akaleta upepo toka mashariki, ukavuma juu ya nchi mchana kutwa na usiku kucha. Kulipokucha, ule upepo ukawa umeleta nzige. Hao nzige wakaenea kila mahali nchini Misri, wakatua juu ya ardhi yote. Nzige hao walikuwa kundi kubwa kupindukia, kiasi ambacho hakijapata kutokea wala hakitatokea tena. Waliifunika nchi yote ya Misri, hata ardhi ikaonekana kuwa giza. Walikula mimea yote na matunda yote yaliyosalia wakati wa ile mvua ya mawe. Hakuna hata jani moja lililosalia nchini. Hakuna jani lolote lililosalia juu ya miti wala mimea popote katika nchi yote ya Misri. Hapo Farao akawaita Mose na Aroni kwa haraka, akawaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na dhidi yenu. Kwa hiyo sasa ninawasihi mnisamehe dhambi yangu, mara hii moja tu, mkaniombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki.” Basi, Mose akaondoka kwa Farao, akaenda kumwomba Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu akaleta upepo mkali toka magharibi, ukawainua wale nzige na kuwasukumia kwenye bahari ya Shamu. Hakuna hata nzige mmoja aliyebaki katika nchi nzima ya Misri. Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, naye hakuwaachia Waisraeli waondoke. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu mbinguni ili giza nene litokee nchini Misri, giza nene ambalo mtu ataweza kulipapasa.” Basi, Mose akanyosha mkono wake juu mbinguni, kukawa na giza nene kote nchini Misri kwa muda wa siku tatu. Watu hawakuweza kuonana wala kuondoka mahali walipokuwa kwa muda huo wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga huko Gosheni walimokuwa wanakaa. Kisha, Farao akamwita Mose, akamwambia, “Nendeni mkamtumikie Mwenyezi-Mungu. Watoto wenu pia wanaweza kwenda pamoja nanyi. Lakini kondoo na mbuzi, na ng'ombe wenu wabaki.” Lakini Mose akamwambia, “Ni lazima uturuhusu kuchukua wanyama wa tambiko na sadaka za kuteketezwa ili tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Ngombe wetu ni lazima pia tuwachukue wala hakuna hata ukwato mmoja utakaobaki nyuma, kwa sababu kutoka katika mifugo yetu wenyewe, tutamtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala sisi hatujui ni mnyama yupi tutakayemtolea Mwenyezi-Mungu tambiko mpaka tutakapofika huko.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, akakataa kuwaachia Waisraeli waondoke. Farao akamwambia Mose, “Toka mbele yangu. Jihadhari sana. Usije kuniona tena, maana siku utakapokuja tena mbele yangu, utakufa!” Mose naye akamwambia, “Sawa! Kama ulivyosema sitakuja kukuona tena.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Bado kuna pigo moja nitakalomletea Farao na nchi ya Misri. Baadaye atawaacheni mwondoke hapa. Tena atakapowaacheni mwondoke, yeye mwenyewe atawafukuza mwondoke kabisa. Waambie Waisraeli sasa wasikie vizuri kwamba kila mmoja wao, mwanamume kwa mwanamke, ni lazima amwombe jirani yake vito vya fedha na dhahabu.” Mwenyezi-Mungu akawafanya Waisraeli wapendeke mbele ya Wamisri. Tena, Mose mwenyewe akawa mtu mashuhuri sana nchini Misri, na mbele ya maofisa wa Farao na watu wote. Mose akamwambia Farao, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Panapo usiku wa manane leo, nitapitia katikati ya nchi ya Misri. Nitakapopita, kila mzaliwa wa kwanza nchini Misri atakufa: Kuanzia mzaliwa wa kwanza wako wewe Farao ambaye ni mrithi wako, hadi mzaliwa wa kwanza wa mjakazi anayesaga nafaka kwa jiwe. Hata wazaliwa wa kwanza wa mifugo nao wote watakufa. Kutakuwa na kilio kikubwa kote nchini Misri, kilio ambacho hakijapata kutokea, wala hakitatokea tena. Lakini miongoni mwa Waisraeli hakuna mtu, mnyama au mbwa wao atakayepatwa na madhara yoyote, ili upate kutambua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu hutofautisha kati ya Waisraeli na Wamisri.’” Mose akamalizia kwa kumwambia Farao, “Watumishi wako hawa watanijia na kuinama mbele yangu kwa heshima, wakinisihi niondoke nchini Misri, mimi pamoja na watu wote wanaonifuata. Baada ya hayo, nitaondoka.” Kisha Mose, huku akiwa ameghadhabika, akaondoka kwa Farao. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Farao hatakusikiliza, ili maajabu yangu yapate kuongezeka nchini Misri.” Basi, Mose na Aroni walifanya maajabu hayo yote mbele ya Farao. Lakini Mwenyezi-Mungu alimfanya Farao kuwa mkaidi, akakataa kuwaruhusu Waisraeli waondoke nchini mwake. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, walipokuwa bado nchini Misri, “Mwezi huu utakuwa kwenu mwezi wa kwanza wa mwaka. Iambieni jumuiya yote ya Waisraeli kwamba mnamo siku ya kumi ya mwezi huu, mtachukua mwanakondoo mmoja kwa kila jamaa moja. Kama jamaa moja ni ndogo mno hata isiweze kumaliza kondoo mmoja, itashirikiana na jamaa jirani kadiri ya idadi ya watu wake; kisha watachagua mnyama ambaye kila mtu ataweza kula. Mwanakondoo huyo asiwe na kilema chochote, awe wa kiume na wa mwaka mmoja. Anaweza kuwa mwanakondoo au mwanambuzi. Mtamweka mnyama huyo mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi huu. Siku hiyo, jumuiya yote ya Waisraeli watawachinja wanyama hao wakati wa jioni. Kisha, watachukua damu ya hao wanyama na kupaka kwenye miimo na vizingiti vya kila nyumba watakamolia wanyama hao. Wataila nyama hiyo usiku huohuo baada ya kuichoma; wataila pamoja na mkate usiotiwa chachu na mboga chungu za majani. Imekatazwa kuila ikiwa mbichi au imechemshwa kwa maji, bali lazima ichomwe yote, pamoja na kichwa, miguu na nyama zake za ndani. Hali kadhalika msibakize nyama yoyote mpaka asubuhi. Nyama yoyote itakayobaki hadi asubuhi mtaiteketeza motoni. Na hivi ndivyo mtakavyomla mnyama huyo: Mtakuwa mmejifunga mikanda viunoni mwenu, mmevaa viatu na fimbo zenu mikononi. Tena mtamla kwa haraka. Hiyo ni Pasaka ya Mwenyezi-Mungu. “Usiku huo, nitapita katika nchi ya Misri na kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Misri, watu kwa wanyama. Nitaiadhibu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. Basi, ile damu itakuwa ishara yenu ya kuonesha nyumba mtakamokuwa. Nami nitakapoiona hiyo damu, nitawapita nyinyi, na hamtapatwa na dhara lolote wakati nitakapoipiga nchi ya Misri. Vizazi hata vizazi mtaadhimisha tukio hilo kwa sikukuu kubwa kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Hilo litakuwa agizo la milele kwenu.” Mwenyezi-Mungu akasema, “Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Siku ya kwanza ya siku hizo saba, mtaondoa chachu katika nyumba zenu. Mtu yeyote akila kitu kilichotiwa chachu katika muda huo wa siku saba, ni lazima aondolewe miongoni mwa Waisraeli. Siku ya kwanza na siku ya saba mtakuwa na mkutano mtakatifu. Katika siku hizo mbili hamtaruhusiwa kufanya kazi yoyote isipokuwa kazi ya lazima ya kutayarisha chakula. Mtaadhimisha sikukuu hii ya mikate isiyotiwa chachu kama ukumbusho wa siku nilipowatoa nyinyi, vikundi vya Israeli, kutoka Misri. Sikukuu hiyo itaadhimishwa na vizazi vyenu vyote vijavyo, kama agizo la milele. Basi, mtakula mikate isiyotiwa chachu kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, mpaka jioni ya siku ya ishirini na moja ya mwezi huohuo wa kwanza. Katika siku hizo saba, msiwe na chachu yoyote katika nyumba zenu. Mtu yeyote, awe mgeni au mwenyeji, akila kitu kilichotiwa chachu, ataondolewa miongoni mwa jumuiya ya Waisraeli. Popote pale mnapoishi, ni mwiko kabisa kula chochote kilichotiwa chachu. Mnapaswa kula mikate isiyotiwa chachu.” Basi, Mose akawaita wazee wote wa Waisraeli, akawaambia, “Chagueni kila mmoja wenu, kulingana na jamaa yake, mwanakondoo na kumchinja kwa sikukuu ya Pasaka. Mtachukua majani ya husopo na kuyachovya katika damu ndani ya birika na kupaka kwenye vizingiti na miimo yote miwili ya milango ya nyumba zenu. Mtu yeyote asitoke nje ya nyumba usiku huo hadi asubuhi. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nitapita kuwaua Wamisri. Lakini nitakapoiona damu iliyopakwa kwenye vizingiti na miimo ya nyumba zenu, nitazipita na wala sitamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwaua. Shikeni jambo hilo nyinyi na wazawa wenu kama agizo la milele. Mtakapoingia katika nchi ile ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nitawapa, kama nilivyoahidi, ni lazima kulitekeleza. Kila wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Jambo hili lina maana gani?’ Nyinyi mtawajibu, ‘Hii ni tambiko ya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu alizipita nyumba za Waisraeli nchini Misri alipowaua Wamisri, lakini sisi hakutuua.’” Waisraeli wakainamisha vichwa na kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Kisha Waisraeli wakaenda, wakafanya kama walivyoambiwa na Mose na Aroni kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu. Mnamo usiku wa manane, Mwenyezi-Mungu aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Misri. Wote walikufa, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa gerezani. Hata wazaliwa wa kwanza wa wanyama nao walikufa. Basi Farao, watumishi wake na wakazi wote wa Misri wakaamka usiku. Kukawa na kilio kikubwa nchini kote Misri kwa maana hapakuwa hata nyumba moja ambamo hakufa mtu. Hapo Farao akawaita Mose na Aroni, usiku huohuo, akamwambia, “Amkeni! Ondokeni miongoni mwa watu wangu. Nendeni, nyinyi pamoja na hao Waisraeli, mkamtumikie Mwenyezi-Mungu kama mlivyosema. Chukueni makundi yenu ya kondoo na ng'ombe, mwondoke; niombeeni na mimi baraka.” Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke haraka, wakisema, “Hakika tutakufa sote!” Basi, Waisraeli wakauchukua unga wao uliokandwa kabla haujatiwa chachu, na mabakuli yao ya kukandia wakiwa wamezifunga kwa nguo na kubeba mabegani. Waisraeli walikuwa wamekwisha fanya kama Mose alivyowaagiza hapo awali: Waliwaomba Wamisri wawapatie vito vya fedha, dhahabu na mavazi. Naye Mwenyezi-Mungu alikwisha wafanya Waisraeli wapendwe na Wamisri, nao Wamisri wakawapa kila kitu walichoomba. Ndivyo Waisraeli walivyowapokonya Wamisri mali yao. Waisraeli waliondoka mjini Ramesesi, wakasafiri kwa miguu kuelekea Sukothi. Walikuwa wanaume wapatao 600,000, licha ya wanawake na watoto. Kulikuwa pia na kundi la watu wengine walioandamana nao pamoja na mifugo mingi, kondoo na ng'ombe. Kwa kuwa walikuwa wameondoka Misri kwa haraka, hawakuweza kutayarisha chakula cha safarini, ila tu ule unga uliokandwa bila kutiwa chachu. Basi, wakaoka mikate isiyotiwa chachu. Waisraeli walikuwa wameishi nchini Misri kwa muda wa miaka 430. Katika siku ya mwisho ya mwaka wa 430, siku hiyohiyo maalumu ndipo makabila yote ya Mwenyezi-Mungu yaliondoka nchini Misri. Usiku huo ambao Mwenyezi-Mungu alikesha ili kuwatoa Waisraeli nchini Misri, unapaswa kuadhimishwa na Waisraeli wote na vizazi vyao vyote, kama usiku wa kukesha kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Yafuatayo ni maagizo juu ya adhimisho la Pasaka. Mgeni yeyote hatashiriki chakula cha Pasaka. Lakini mtumwa yeyote aliyenunuliwa kwa fedha, baada ya kumtahiri, ataruhusiwa kushiriki. Msafiri yeyote, wala kibarua yeyote, hatashiriki chakula hicho. Mwanakondoo wa Pasaka ataliwa katika nyumba moja. Hamtatoa nyama yoyote nje ya nyumba alimochinjiwa, wala hamtavunja hata mfupa mmoja wa mnyama wa Pasaka. Jumuiya yote ya watu wa Israeli itaadhimisha sikukuu hiyo. Mgeni yeyote anayeishi miongoni mwenu akipenda kuadhimisha sikukuu ya Pasaka, ni lazima kwanza wanaume wote wa nyumba yake watahiriwe; hapo atahesabiwa kuwa kama mwenyeji na kuruhusiwa kushiriki. Mwanamume yeyote asiyetahiriwa asishiriki kamwe. Sheria zilezile zitamhusu mzalendo Mwisraeli na wageni watakaoishi miongoni mwenu”. Waisraeli wote walitii sheria hiyo na kufanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaagiza Mose na Aroni. Siku hiyohiyo Mwenyezi-Mungu aliwatoa Waisraeli nchini Misri kwa makundi. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Niwekee wakfu wazaliwa wote wa kwanza wa kiume, maana wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa Waisraeli na kila wazaliwa wa kwanza wa wanyama ni wangu.” Mose akawaambia watu, “Ikumbukeni siku hii mliyotoka nchini Misri ambako mlikuwa watumwa. Hii ndiyo siku Mwenyezi-Mungu alipowatoa humo kwa mkono wake wenye nguvu. Katika siku hii, kamwe msile mkate uliotiwa chachu. Siku hii, mwezi wa kwanza wa Abibu, mtaondoka nchini Misri. Na wakati Mwenyezi-Mungu atakapowafikisha katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Wahivi na Wayebusi, nchi ambayo aliwaapia babu zenu kwamba atawapa nyinyi, nchi inayotiririka maziwa na asali, ni lazima muiadhimishe sikukuu hii kila mwaka katika mwezi huu wa kwanza. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, na mnamo siku ya saba mtafanya sikukuu kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu. Kwa muda huo wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Kusiwepo na mikate iliyotiwa chachu, wala chachu yoyote miongoni mwenu na katika nchi yenu yote. Siku hiyo mtawaambia watoto wenu kwamba mnafanya hivyo kwa sababu ya jambo alilowafanyia Mwenyezi-Mungu mlipoondoka nchini Misri. Adhimisho hilo litakuwa ukumbusho, kama alama katika mikono yenu au katika paji la nyuso zenu; ili iwakumbushe daima sheria ya Mwenyezi-Mungu. Maana, Mwenyezi-Mungu amewatoa nchini Misri kwa mkono wenye nguvu. Kwa hiyo, mtaadhimisha sikukuu hii kwa wakati uliopangwa, kila mwaka.” Mose akaendelea kuwaambia watu, “Hali kadhalika, wakati Mwenyezi-Mungu atakapowafikisha katika nchi ya Wakanaani na kuwapeni iwe mali yenu kama alivyowaapia nyinyi na babu zenu, lazima kumwekea Mwenyezi-Mungu kila mzaliwa wenu wa kwanza wa kiume. Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mifugo yenu atakuwa wa Mwenyezi-Mungu. Lakini mzaliwa wa kwanza wa kiume wa punda utamkomboa kwa kulipa mwanakondoo, la sivyo, utamuua kwa kumvunja shingo. Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa binadamu utamkomboa. Kama hapo baadaye mwanao akiuliza maana ya jambo hili, utamwambia, ‘Kwa nguvu ya mkono wake, Mwenyezi-Mungu alitutoa nchini Misri ambako tulikuwa watumwa. Farao kwa ukaidi alikataa kutuachia tuondoke; kwa hiyo Mwenyezi-Mungu alimuua kila mzaliwa wa kwanza nchini Misri, mzaliwa wa kwanza wa binadamu na wa mnyama. Basi, mimi ninamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mifugo yangu, lakini kila mzaliwa wa kwanza wa wanangu namkomboa.’ Jambo hili litakuwa kama alama mkononi mwako au utepe katika paji la uso wako, kwamba Mwenyezi-Mungu alitutoa nchini Misri kwa mkono wenye nguvu.” Wakati Farao alipowaachia Waisraeli waende zao, Mungu hakuwapitisha katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa ya karibu. Mungu alisema, “Sipendi watu hawa wabadilishe nia na kurudi Misri wakijua itawabidi kupigana vita.” Badala yake, Mungu aliwapitisha Waisraeli katika njia ya mzunguko kupitia jangwani, kuelekea bahari ya Shamu. Waisraeli waliondoka nchini Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita. Mose aliichukua mifupa ya Yosefu kama Yosefu alivyoagiza kabla ya kufa kwake. Alikuwa amewaapisha rasmi Waisraeli akisema, “Mungu atakapowajia kuwatoa nchini humu, ni lazima mwichukue mifupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.” Basi, Waisraeli waliondoka Sukothi, wakapiga kambi huko Ethamu, ukingoni mwa jangwa. Mchana Mwenyezi-Mungu aliwatangulia katika mnara wa wingu kuwaonesha njia, na usiku aliwatangulia katika mnara wa moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana na usiku. Mnara wa wingu wakati wa mchana, na mnara wa moto wakati wa usiku, kamwe haikukosekana kuwatangulia Waisraeli. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli warudi nyuma, wapige kambi mbele ya Pi-hahirothi, kati ya mji wa Migdoli na bahari ya Shamu, mbele ya Baal-sefoni. Mtapiga kambi mbele yake karibu na bahari. Maana, Farao atafikiri, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga, nalo jangwa limewazuia wasiweze kutoka.’ Hapo mimi nitamfanya Farao kuwa mkaidi, naye atawafuatia. Nami nitajipatia utukufu kwa kumwangamiza yeye na jeshi lake. Hapo Wamisri watatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Waisraeli wakafanya hivyo. Farao, mfalme wa Misri, aliposikia kwamba Waisraeli wamekimbia, yeye na maofisa wake walibadili fikira zao, wakasema, “Tumefanya nini kuwaachia Waisraeli waende zao wasitutumikie tena?” Basi, Farao akatayarisha gari lake la vita na jeshi lake. Alichukua magari yake bora ya vita 600 na magari yote mengine ya kivita ya Misri yakiongozwa na maofisa wa kijeshi. Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao, mfalme wa Misri, kuwa mkaidi naye akawafuatia Waisraeli ambao walikuwa wameondoka Misri kwa ushupavu. Wamisri pamoja na farasi wao wote, magari ya farasi ya vita na wapandafarasi wake waliwafuata Waisraeli, wakawakuta wamepiga kambi kando ya bahari, karibu na Pi-hahirothi, mbele ya Baal-sefoni. Waisraeli walipotazama na kumwona Farao akija na jeshi lake dhidi yao, walishikwa na hofu kubwa, wakamlilia Mwenyezi-Mungu. Wakamwambia Mose, “Je, hapakuwa na makaburi ya kutosha nchini Misri hata ukatuleta tufie huku jangwani? Mbona umetutendea haya, kwa tututoa katika nchi ya Misri? Je, hatukukuambia mambo haya tulipokuwa bado Misri? Tulikuambia utuache tuendelee kuwatumikia Wamisri. Ingalikuwa afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufia huku jangwani.” Mose akawaambia Waisraeli, “Msiogope! Kaeni imara! Leo mtaona jinsi Mwenyezi-Mungu atakavyowaokoa. Maana, hawa Wamisri mnaowaona leo, hamtawaona tena. Mwenyezi-Mungu atawapigania; nyinyi mnachotakiwa kufanya ni kutulia tu.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa nini mnanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele. Inua fimbo yako na kuinyosha juu ya bahari. Maji yatagawanyika na Waisraeli wataweza kuvuka katikati ya bahari mahali pakavu. Mimi nitawafanya Wamisri kuwa wakaidi, nao watawafuatia katikati ya bahari; nami nitajipatia utukufu kutokana na kuangamizwa kwa Farao na jeshi lake, magari yake ya vita pamoja na wapandafarasi wake. Naam, nitatukuka kwa kumwangamiza Farao na jeshi lake, pamoja na magari yake na wapandafarasi; nao Wamisri watajua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, malaika wa Mungu aliyekuwa mbele ya kundi la Waisraeli aliondoka akakaa nyuma yao. Na ule mnara wa wingu pia uliondoka mbele ukasimama nyuma yao, ukakaa katikati ya Waisraeli na Wamisri. Lile wingu likawatia Wamisri giza, lakini likawaangazia Waisraeli usiku. Kwa hiyo, makundi hayo mawili, jeshi la Farao na kundi la Waisraeli, hayakukaribiana usiku kucha. Mose akaunyosha mkono wake juu ya bahari, naye Mwenyezi-Mungu akaisukuma bahari nyuma kwa upepo mkali toka mashariki. Upepo huo ulivuma usiku kucha, ukaigawa bahari sehemu mbili na katikati kukatokeza nchi kavu. Waisraeli wakapita katikati ya bahari mahali pakavu, kuta za maji zikiwa upande wao wa kulia na wa kushoto. Wamisri wakawafuata kwa kupitia nchi kavu iliyokuwa katikati ya bahari pamoja na farasi wao, magari yao ya vita na wapandafarasi wao wote. Karibu na mapambazuko, Mwenyezi-Mungu aliliangalia jeshi la Wamisri kutoka katika ule mnara wa moto na ule mnara wa wingu, akalitia hofu kubwa. Aliyakwamisha magurudumu ya magari yao, yakawa yakienda kwa shida sana. Hapo Wamisri wakasema, “Tuwakimbie Waisraeli; Mwenyezi-Mungu anawapigania Waisraeli dhidi yetu.” Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi na kuwafunika Wamisri pamoja na magari yao na wapandafarasi wao.” Basi, Mose akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka bahari ikarudia hali yake ilivyokuwa. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji lakini Mwenyezi-Mungu akawasukumizia baharini. Maji yakayafunika magari pamoja na wapandafarasi; jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuatia Waisraeli likafa baharini. Hakunusurika Mmisri hata mmoja. Lakini Waisraeli walipita katikati ya bahari mahali pakavu, kuta za maji zikiwa zimesimama upande wao wa kulia na wa kushoto. Siku hiyo Mwenyezi-Mungu aliwaokoa Waisraeli mikononi mwa Wamisri; nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni wamekufa. Waisraeli walipoona tendo hilo la ajabu alilofanya Mwenyezi-Mungu dhidi ya Wamisri, wakamcha, wakawa na imani na Mwenyezi-Mungu na Mose mtumishi wake. Hapo, Mose pamoja na Waisraeli wakamwimbia Mwenyezi-Mungu wimbo huu, “Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu kwani ameshinda kwa fahari, farasi na mpandafarasi wake amewatosa baharini. Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu na uwezo, yeye mwenyewe ndiye anayeniokoa. Yeye ni Mungu wangu nami nitamsifu, ni Mungu wa baba yangu nami nitamtukuza. Mwenyezi-Mungu ni shujaa vitani; Mwenyezi-Mungu ndilo jina lake. “Magari na majeshi ya Farao ameyatumbukiza baharini, maofisa wake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. Vilindi vya maji vimewafunika, wameporomoka baharini kama jiwe. “Mkono wako wa kulia ee Mwenyezi-Mungu watukuka kwa nguvu; kwa mkono wako wa kulia ee Mwenyezi-Mungu wawaponda adui. Kwa wingi wa ukuu wako wawaangamiza wapinzani wako; wawapulizia ghadhabu yako nayo yawateketeza kama makapi. Kwa pumzi ya pua yako maji yalirundikana, mawimbi yakasimama wima kama ukuta; vilindi katikati ya bahari vikagandamana. Adui alijisemea, ‘Nitawafuata na kuwakamata; nitagawanya nyara mpaka hamu yangu iishe. Tutaufuta upanga wetu, tutawaangamiza kwa mkono wetu.’ Lakini wewe uliuvumisha upepo wako, nayo bahari ikawafunika. Walizama majini kama risasi. “Ewe Mwenyezi-Mungu, ni nani kati ya miungu anayelingana nawe? Ni nani aliye kama wewe uliye mtakatifu mkuu, utishaye kwa matendo matukufu, unayetenda mambo ya ajabu? Uliunyosha mkono wako wa kulia, nayo nchi ikawameza maadui zetu. “Kwa fadhili zako kuu umewaongoza watu uliowakomboa, kwa nguvu yako umewaongoza kwenye makao yako matakatifu. Watu wa mataifa wamesikia hayo wakatetemeka; wakazi wa Filistia wamekumbwa na kitisho. Wakuu wa Edomu wamefadhaishwa; viongozi wa Moabu wamekumbwa na woga mkuu; wakazi wote wa Kanaani wamevunjika moyo. Kitisho na hofu vimewavamia. Kwa sababu ya ukuu wa nguvu zako, wao wamenyamaza kimya kama jiwe, mpaka watu wako ee Mwenyezi-Mungu, wapite, naam, mpaka watu hao uliowakomboa wamewapita. Wewe utawaleta watu wako na kuwapanda mlimani pako; pale ulipochagua ee Mwenyezi-Mungu pawe makao yako, mahali patakatifu ee Mwenyezi-Mungu ulipojenga kwa mikono yako. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, watawala milele na milele.” Wakati farasi wa Farao na magari yake pamoja na wapandafarasi wake walipoingia mahali pakavu baharini, Mwenyezi-Mungu aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika. Lakini Waisraeli waliendelea kutembea pakavu katikati ya bahari. Basi nabii Miriamu, dada yake Aroni, akachukua kingoma mkononi, na wanawake wengine wote wakamfuata wakiwa na vingoma vyao wakicheza. Miriamu akawaongoza kwa kuimba, “Mwimbieni Mwenyezi-Mungu kwani ameshinda kwa fahari, farasi na mpandafarasi wake amewatosa baharini.” Kisha, Mose aliwaongoza Waisraeli kutoka bahari ya Shamu, wakaenda mpaka jangwa la Shuri. Walisafiri kwa muda wa siku tatu jangwani bila kuona maji yoyote. Walipofika mahali panapoitwa Mara, hawakuweza kuyanywa maji ya Mara kwa sababu yalikuwa machungu. Kwa sababu hiyo mahali hapo pakaitwa Mara. Basi, watu wote wakamlalamikia Mose wakisema, “Sasa tutakunywa nini?” Hapo Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamwonesha kipande cha mti, na Mose akakitumbukiza katika maji; maji hayo yakawa mazuri. Huko Mungu aliwapa Waisraeli amri na agizo, ili ajue uthabiti wao, akawaambia, “Ikiwa mtaisikiliza kwa makini sauti yangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kutenda yaliyo sawa mbele yangu, na kuheshimu amri na maagizo yangu yote, basi, mimi sitawaletea yale magonjwa niliyowaletea Wamisri. Kwa sababu, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu ninayewaponya nyinyi.” Kisha Waisraeli wakawasili huko Elimu ambako kulikuwa na chemchemi kumi na mbili na mitende sabini. Wakapiga kambi yao huko karibu na maji. Jumuiya yote ya Waisraeli iliondoka, ikafika jangwa la Sini kati ya Elimu na Sinai. Hii ilikuwa siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili tangu walipoondoka nchini Misri. Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikawalalamikia Mose na Aroni huko jangwani, “Laiti Mwenyezi-Mungu angelituua tulipokuwa nchini Misri ambako tulikaa, tukala nyama na mikate hata tukashiba. Lakini nyinyi mmetuleta huku jangwani kuiua jumuiya hii yote kwa njaa!” Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mimi nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Kila siku watu watatoka na kukusanya chakula cha siku hiyo. Kwa njia hii nitawajaribu nione kama watazifuata sheria zangu au hawatazifuata. Lakini siku ya sita, wakati watakapoandaa chakula walichokusanya, kiasi hicho kitakuwa mara mbili ya chakula cha kila siku.” Basi, Mose na Aroni wakawaambia watu wote wa Israeli, “Jioni, mtatambua kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye aliyewatoa nchini Misri! Tena, kesho asubuhi, mtauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie?” Tena Mose akasema, “Jioni, Mwenyezi-Mungu atawapeni nyama mle, na asubuhi atawapeni mikate mle mshibe, maana yeye ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie? Msitunungunikie sisi bali mnungunikieni Mwenyezi-Mungu.” Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli ikusanyike mbele ya Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko yenu.” Wakati Aroni alipokuwa akizungumza na jumuiya ya Waisraeli, watu wote walitazama huko jangwani, na mara utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukaonekana mawinguni. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nimeyasikia manunguniko ya Waisraeli. Basi, waambie kwamba wakati wa jioni watakula nyama, na asubuhi watakula mkate. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Basi, mnamo wakati wa jioni kukaja kware wengi, wakafunika kambi ya Waisraeli. Asubuhi yake kukatokea umande, ukatanda kandokando ya kambi yao. Umande huo ulipotoweka, kukabaki huko nyikani kitu kama mkate mwembamba na mwepesi. Waisraeli walipoona kitu hicho walishangaa, wakaulizana, “Nini hiki?” Hawakujua kilikuwa kitu gani. Basi, Mose akawaambia, “Huu ni mkate ambao Mwenyezi-Mungu amewapa mle. Mwenyezi-Mungu ameamuru mfanye hivi: Kila mtu na akusanye chakula kiasi anachoweza kula; ataokota kiasi cha pishi moja kwa kila mtu hemani mwake.” Basi, Waisraeli wakafanya hivyo, na ikawa kwamba, wengine waliokota kwa wingi na wengine kidogo. Lakini wote walipokipima kipimo walichookota katika pishi, waligundua kuwa aliyeokota kingi hakuwa na cha ziada, na aliyeokota kidogo, hakupungukiwa. Kila mmoja alikuwa ameokota kiasi alichoweza kula. Mose akawaambia watu, “Mtu yeyote asibakize chakula hicho mpaka asubuhi.” Lakini watu hawakumsikiliza Mose. Baadhi yao walijibakizia chakula mpaka asubuhi. Lakini asubuhi chakula hicho kikawa kimeoza na kuwa na mabuu. Mose akawakasirikia sana watu. Basi, kila asubuhi walikusanya chakula kila mtu kiasi alichohitaji kula. Jua lilipopanda juu na kuwa kali, kile chakula kingine kiliyeyuka. Katika siku ya sita, Waisraeli walikusanya chakula hicho maradufu, pishi nne kwa kila mtu. Basi, wazee wote wa jumuiya ya Waisraeli walimwendea Mose, wakamweleza jambo hilo. Mose akawaambia, “Hii ndiyo amri ya Mwenyezi-Mungu. Kesho ni siku rasmi ya mapumziko; ni Sabato takatifu ya Mwenyezi-Mungu. Basi, nendeni mkapike au mkachemshe kile chakula mnachohitaji leo, na chakula kitakachosalia kiwekeni mpaka kesho.” Basi, wakafanya hivyo na kukiacha chakula kingine mpaka kesho yake kama Mose alivyosema. Asubuhi yake waliona kwamba hakikuharibika wala kuwa na mabuu. Basi, Mose akawaambia, “Kuleni chakula hicho kilichosalia kwa sababu leo ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu. Leo hamtapata chakula huko nje. Kwa siku sita mtakuwa mkikusanya chakula hiki, lakini siku ya saba ambayo ni Sabato hakitakuwapo.” Mnamo siku ya saba watu kadhaa walitoka kwenda kutafuta chakula, lakini hawakukipata. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mpaka lini mtakataa kuzitii amri na Sheria zangu? Fahamuni kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nimewapa siku ya Sabato, ndiyo maana nikawapa chakula cha siku mbili mnamo siku ya sita. Basi, pumzikeni kila mtu nyumbani mwake; mtu yeyote asitoke katika siku ya saba.” Kwa hiyo, watu walipumzika siku ya saba. Waisraeli walikiita chakula hicho “Mana.” Kilikuwa kama mbegu za mtama mweupe na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotiwa asali. Mose akawaambia, “Hili ndilo agizo la Mwenyezi-Mungu: Chukueni kiasi cha pishi moja ya mana na kuiweka kwa ajili ya wazawa wenu, ili waweze kuona chakula nilichowalisha jangwani wakati nilipowatoa nchini Misri.” Mose akamwambia Aroni, “Chukua gudulia utie ndani pishi moja ya mana na kuiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu, iwe kwa ajili ya wazawa wenu.” Basi, Aroni akaiweka mana mahali patakatifu mbele ya sanduku la agano ili ihifadhiwe kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza Mose. Waisraeli walikula mana kwa muda wa miaka arubaini, mpaka walipofika katika nchi iliyofaa kuishi, nchi iliyokuwako mpakani mwa Kanaani ambako walifanya makao yao. (Posho ya mana, kiasi cha pishi nne, ilikuwa sehemu ya kumi ya kipimo cha kawaida kiitwacho efa.) Kutoka jangwa la Sini, jumuiya yote ya Waisraeli ilisafiri hatua kwa hatua kama alivyoamuru Mwenyezi-Mungu, watu wakapiga kambi huko Refidimu. Lakini huko hakukuwa na maji ya kunywa. Kwa hiyo watu wakamnungunikia Mose wakisema, “Tupe maji ya kunywa.” Mose akawauliza, “Mbona mnaninungunikia? Mbona mnamjaribu Mwenyezi-Mungu?” Lakini wote walikuwa na kiu, wakamnungunikia Mose wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri utuue kwa kiu sisi sote na watoto wetu na mifugo yetu?” Basi, Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nitawafanyia nini watu hawa? Wako karibu kunipiga mawe!” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Pita mbele ya watu hawa ukiwachukua wazee wao kadhaa; chukua pia mkononi mwako ile fimbo uliyoipiga nayo mto Nili. Tazama mimi nitasimama mbele yako mwambani pale Horebu, nawe utaupiga huo mwamba na maji yatabubujika kutoka humo ili watu wote wapate kunywa.” Basi, Mose akafanya hivyo mbele ya wazee wa Waisraeli. Mahali hapo Mose akapaita “Masa” na “Meriba”, kwa sababu Waisraeli walimnungunikia na kumjaribu Mwenyezi-Mungu wakisema, “Je, kweli Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi?” Waamaleki walikuja na kupigana na Waisraeli huko Refidimu. Mose akamwambia Yoshua, “Chagua wanaume uende ukapigane na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilele cha kilima, nikiishika mkononi mwangu ile fimbo ya Mungu.” Basi, Yoshua akafanya kama Mose alivyosema, akaenda kupigana na Waamaleki. Mose, Aroni na Huri wakapanda kilele cha kilima. Ikawa wakati wote Mose alipoinua mkono wake juu, Waisraeli walishinda, na alipouteremsha, Waamaleki walishinda. Lakini baada ya muda, mikono ya Mose ilichoka. Kwa hiyo Aroni na Huri walichukua jiwe wakaliweka karibu na Mose naye akaketi. Kisha wakaishika na kuiinua mikono yake, mmoja akauinua mkono wa kulia na mwingine mkono wa kushoto. Hivyo mikono ya Mose ikabaki imara ikiwa imeinuliwa juu hadi jua lilipotua. Yoshua akawakatakata Waamaleki. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Liandike jambo hili katika kitabu, liwe ukumbusho. Tena kariri masikioni mwa Yoshua kwamba nitawafuta kabisa Waamaleki duniani.” Mose akajenga madhabahu na kuiita, “Mwenyezi-Mungu ni Bendera Yangu”, akisema, “Inueni juu bendera ya Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu atapigana na Waamaleki kizazi hata kizazi!” Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Mose, alisikia juu ya mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimtendea Mose na Waisraeli alipowatoa katika nchi ya Misri. Kwa hiyo Yethro, akiwa na Sipora, mkewe Mose, ambaye Mose alikuwa amemrudisha kwa baba yake, alimwendea Mose, pamoja na watoto wawili wa Mose. Mtoto wa kwanza aliitwa Gershomu. Mose alimpa jina hili kwa vile alisema, “Nimekimbilia katika nchi ya kigeni.” Wa pili aliitwa Eliezeri, kwa vile Mose alisema, “Mungu wa baba yangu ndiye aliyenisaidia nisiuawe na Farao.” Yethro, mkwewe Mose, alikuja pamoja na binti yake, yaani mkewe Mose, pamoja na watoto, akamkuta Mose jangwani alikokuwa amepiga kambi kwenye mlima wa Mungu. Mose alipoambiwa kuwa baba mkwe wake pamoja na mkewe na wanawe wawili wanakuja, alitoka kwenda kumlaki baba mkwe wake, akamwinamia na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani. Mose akamweleza mkwewe mambo yote Mwenyezi-Mungu aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Waisraeli. Alimwambia pia juu ya shida zote zilizowapata safarini na jinsi Mwenyezi-Mungu alivyowaokoa. Yethro akafurahishwa na yote aliyotenda Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya Waisraeli, kwa kuwaokoa mikononi mwa Wamisri. Yethro akasema, “Na atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewaokoa mikononi mwa Wamisri na kutoka utumwa wa Farao. Sasa najua kwamba Mwenyezi-Mungu ni mkuu kuliko miungu yote, kwani amewakomboa watu hawa mikononi mwa Wamisri ambao waliwatendea ujeuri.” Hapo Yethro, baba mkwe wa Mose, akamtolea Mungu sadaka za kuteketezwa na tambiko. Naye Aroni akaja pamoja na wazee wa Israeli ili kula chakula pamoja na Yethro, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kesho yake, Mose aliketi kuamua matatizo ya Waisraeli, nao wakasimama wakiwa wamemzunguka, tangu asubuhi mpaka jioni. Yethro, baba mkwe wa Mose, alipoyaona mambo yote ambayo Mose aliwafanyia Waisraeli, alimwuliza, “Kwa nini unawafanyia watu mambo haya? Mbona unaketi peke yako huku watu wamekuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?” Mose akamjibu mkwewe, “Kwa sababu watu huja kwangu kuuliza matakwa ya Mungu. Wakiwa na ugomvi wowote ule wao huja kwangu nami huamua kati ya mtu na mwenzake, na kuwafunza amri za Mungu na maamuzi yake.” Basi, Yethro akamwambia Mose, “Unavyofanya si vizuri! Utajidhuru mwenyewe na hawa watu kwa uchovu, kwani hii ni kazi ngumu usiyoweza kuifanya peke yako. Sikiliza shauri langu kwako, na Mungu awe pamoja nawe. Wewe utawawakilisha watu mbele ya Mungu na kumletea Mungu matatizo yao. Hali kadhalika utawafundisha amri na maamuzi ya Mungu na kuwaonesha jinsi inavyowapasa kuishi na kufanya. Lakini kuhusu mambo mengine, chagua miongoni mwa watu wote, watu wanaostahili, watu wanaomcha Mungu, waaminifu na wanaochukia kuhongwa. Wape hao mamlaka, wawe na jukumu la kuwasimamia watu katika makundi ya watu elfu, mia, hamsini na kumikumi. Hao ndio watakaokuwa na vikao kila siku kutatua matatizo ya watu. Matatizo magumu watakuletea wewe, lakini yale madogomadogo watayaamua wenyewe. Kwa njia hiyo utaweza kurahisisha kazi yako kwa vile watashirikiana nawe katika jukumu hilo. Ukifanya hivyo, na kama ndivyo atakavyo Mungu, utaweza kustahimili na watu hawa wote wataweza kurudi makwao kwa amani.” Mose alilisikiliza shauri hilo la mkwewe na kufanya kama alivyoshauriwa. Basi, akawateua watu wenye uwezo kati ya Waisraeli, akawafanya kuwa viongozi wa makundi ya watu elfu, watu mia, watu hamsini na watu kumikumi. Nao wakawa wanaamua matatizo ya watu kila wakati. Matatizo magumu walimletea Mose, lakini yale madogomadogo waliyatatua wao wenyewe. Baada ya kufanya hivyo, Mose na mkwewe wakaagana naye Yethro akarudi nchini kwake. Siku ya kwanza ya mwezi wa tatu tangu walipotoka nchini Misri, watu wa Israeli walifika katika jangwa la Sinai. Walipoondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, huko walipiga kambi mbele ya mlima Sinai. Basi, Mose akapanda juu mlimani kwa Mungu. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwita Mose kutoka huko juu mlimani, akamwambia, “Hivi ndivyo utakavyowaambia wazawa wa Yakobo, hao Waisraeli, ‘Nyinyi wenyewe mmeona nilivyowatenda Wamisri na jinsi nilivyowachukua kama tai anavyochukua watoto wake kwa mabawa, nikawaleta kwangu. Sasa basi, kama mkiitii sauti yangu na kulishika agano langu, mtakuwa watu wangu wateule kati ya mataifa yote, maana dunia yote ni yangu. Mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Hayo ndiyo maneno utakayowaambia Waisraeli.” Basi, Mose akarudi, akawakusanya pamoja wazee wa Waisraeli na kuwaambia maneno hayo aliyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Watu wote wakaitikia kwa pamoja wakisema, “Mambo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya.” Mose akamjulisha Mwenyezi-Mungu jibu hilo la watu. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Haya, mimi nitakujia katika wingu zito ili Waisraeli wapate kunisikia ninaposema nawe na kukuamini siku zote.” Kisha Mose akamwambia Mungu jinsi watu walivyosema. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa watu uwatakase leo na kesho. Waambie wayafue mavazi yao wawe tayari kwa kesho kutwa, maana siku hiyo ya tatu mimi Mwenyezi-Mungu nitashuka juu ya mlima Sinai mbele ya watu wote. Tena wewe utawawekea watu mpaka kuzunguka mlima. Utawakanya wajihadhari sana wasipande juu mlimani wala kuugusa mpaka wake. Yeyote atakayeugusa mlima, atauawa. Mtu asimguse mtu huyo; atauawa kwa kupigwa mawe au mshale awe ni mtu au ni mnyama, hataishi. Wakati mbiu itakapopigwa mfululizo, watu wote watakaribia mlimani.” Basi, Mose akashuka mlimani na kuwaendea watu, akawatakasa, nao wakayafua mavazi yao. Kisha akawaambia watu wote, “Kesho kutwa muwe tayari, na mwanamume yeyote asimkaribie mwanamke.” Basi, siku ya tatu asubuhi, kukatokea ngurumo na umeme na wingu zito juu ya mlima. Ikasikika pia sauti kubwa ya mbiu ambayo iliwatetemesha watu wote kambini. Kisha Mose akawaongoza watu wote kutoka kambini, wakaenda kukutana na Mungu. Wote walikwenda wakajipanga chini ya mlima. Mlima wa Sinai ulikuwa umefunikwa na moshi kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alishuka juu yake katika moto. Moshi wa moto huo ulipanda juu kama moshi wa tanuri kubwa na mlima wote ulitetemeka kwa nguvu. Sauti ya mbiu ilizidi kuongezeka, na Mose akaongea na Mungu. Mungu naye akamjibu katika ngurumo. Mwenyezi-Mungu alishuka juu ya mlima Sinai, akamwita Mose kutoka huko juu, naye Mose akapanda mlimani. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Shuka chini ukawaonye watu wote wasije kunitazama; la sivyo wengi wao wataangamia. Hata makuhani ambao hunikaribia wanapaswa kujitakasa; la sivyo nitawaadhibu.” Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Watu hawa hawawezi kuupanda mlima wa Sinai kwani wewe mwenyewe ulituamuru tuweke mpaka kuuzunguka mlima.” Mwenyezi-Mungu akasema, “Teremka chini kisha urudi pamoja na Aroni. Lakini usiwaruhusu makuhani na watu wengine wapite mpaka na kuja kwangu, la sivyo nitawaadhibu.” Basi, Mose akashuka na kuwaambia Waisraeli mambo yote aliyoagizwa. Mwenyezi-Mungu alizungumza maneno haya yote, akasema, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa nchini Misri, ambako ulikuwa mtumwa. “Usiwe na miungu mingine ila mimi. “Usijifanyie sanamu ya miungu wa uongo, au kinyago cha chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini chini ya dunia. Usiisujudie wala kuitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu. Nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha hao wanichukiao. Lakini nawafadhili maelfu ya wale wanipendao na kuzishika amri zangu. “Usilitaje bure jina langu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Maana mimi Mwenyezi-Mungu sitaacha kumwadhibu anayetumia jina langu vibaya. “Usisahau kuiweka takatifu siku ya Sabato. Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote. Lakini siku ya saba ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala watumishi wako wa kike, wala mnyama wako wa kufugwa, wala mgeni aliye nyumbani mwako. Maana kwa siku sita mimi Mwenyezi-Mungu niliziumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo, kisha nikapumzika siku ya saba. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu niliibariki siku ya Sabato, nikaitakasa. “Waheshimu baba yako na mama yako, ili uishi maisha marefu katika nchi ninayokupa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. “Usiue. “Usizini. “Usiibe. “Usimshuhudie jirani yako uongo. “Usiitamani nyumba ya jirani yako, wala mke wake, wala mtumwa wake wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala chochote kilicho mali ya jirani yako.” Watu waliposikia ngurumo na kuona umeme ukiwaka na kuisikia sauti ya parapanda juu ya mlima uliokuwa unafuka moshi, wote waliogopa na kutetemeka. Wote walisimama mbali, wakamwambia Mose, “Ongea nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza, lakini Mwenyezi-Mungu asiongee nasi, tusije tukafa.” Mose akawaambia, “Msiogope, maana Mungu amekuja kuwajaribu ili mpate kumcha yeye daima na msitende dhambi.” Watu wote walisimama mbali wakati Mose alipokaribia lile wingu zito alimokuwamo Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli: ‘Mmejionea nyinyi wenyewe kwamba nimeongea nanyi kutoka mbinguni. Mtaniheshimu mimi peke yangu wala msijifanyie miungu ya fedha wala ya dhahabu. Nyinyi mtanijengea madhabahu ya udongo ambayo juu yake mtanitambikia kondoo wenu na ng'ombe wenu kama sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Mahali popote nitakapowakumbusha watu jina langu, papo hapo mimi mwenyewe nitawajia na kuwabariki. Kama mkinijengea madhabahu ya mawe, msiitengeneze kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia vyombo vya kuchongea mawe, mtaitia najisi. Wala msitengeneze madhabahu yenye ngazi za kupandia, mtu asije akauona uchi wa huyo anayepanda juu yake.’ “Haya ndiyo maagizo utakayowapa Waisraeli: Ukimnunua mtumwa Mwebrania, atakutumikia kwa miaka sita, lakini mwaka wa saba atakuwa huru na kuondoka, bila malipo. Kama alinunuliwa kabla hajaoa, ataondoka peke yake. Lakini kama alikuja na mkewe, basi, ataondoka na mkewe. Kama bwana wake alimwoza mke, akamzalia watoto wa kike au wa kiume, basi, huyo mwanamke na watoto wake watakuwa mali ya huyo bwana wake, na huyo mtumwa ataondoka peke yake. Lakini kama mtumwa huyo akisema kwamba anampenda bwana wake, mke wake na watoto wake na hataki kuondoka na kuwa huru, basi, bwana wake atamleta mbele ya Mungu. Kisha atampeleka kwenye mlango au kizingitini na kumtoboa sikio lake kwa shazia; naye atamtumikia bwana wake maisha yake yote. “Mtu akimwuza binti yake kuwa mtumwa, huyo hatapata uhuru wake kama watumwa wa kiume. Ikiwa huyo bwana wake alimnunua awe mmoja wa wake zake, kisha asipendezwe naye, huyo bwana atamwacha baba yake huyo mtumwa amkomboe. Huyo bwana hana haki ya kumwuza kwa watu wa mataifa mengine, kwa kuwa atakuwa amekosa uaminifu. Kama ataamua kumwoza kwa mwanawe, atamtendea mtumwa huyo kama binti yake. Kama huyo bwana akioa mke mwingine, lazima aendelee kumtosheleza mkewe wa kwanza kwa chakula, mavazi na haki zake za ndoa. Iwapo huyo bwana hatamtimizia haki hizo tatu, basi, mke ataondoka na kuwa huru bila malipo yoyote. “Ampigaye mtu na kumwua, lazima auawe. Lakini kama hakuwa amemvizia, bali ni kwa ajali, basi, huyo mwuaji ataweza kukimbilia usalama mahali nitakapowachagulieni. Lakini mtu akimshambulia mwenzake makusudi na kumwua kwa ujeuri, hata kama atakimbilia kwenye madhabahu, mtamtoa huko madhabahuni pangu na kumwua. “Ampigaye baba yake au mama yake lazima auawe. “Amtekaye mtu nyara ili kumwuza au kumfanya mtumwa wake lazima auawe. “Amlaaniye baba yake au mama yake lazima auawe. “Watu wawili wakigombana, kisha mmoja akampiga mwenzake jiwe au ngumi bila kumwua, lakini akamjeruhi kiasi cha kumfanya augue na kulala kitandani, iwapo huyo aliyepigwa atapata nafuu na kuweza kutembea kwa kutegemea fimbo, huyo aliyemjeruhi atasamehewa. Lakini, atamlipa fidia ya muda alioupoteza kitandani, na kuhakikisha amemwuguza mpaka apone kabisa. “Mtu akimpiga mtumwa wake wa kiume au wa kike kwa fimbo na kumwua papo hapo, ni lazima aadhibiwe. Lakini mtumwa huyo akibaki hai siku moja au mbili, bwana wake hataadhibiwa, kwani huyo alikuwa ni mali yake. “Wanaume wakipigana na kumwumiza mwanamke mjamzito, hata mimba yake ikaharibika bila madhara mengine zaidi, yule aliyemwumiza atatozwa faini kama atakavyodai mumewe mwanamke huyo na kama mahakimu watakavyoamua. Lakini kama yatakuwapo madhara mengine, basi, lazima amlipe uhai kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, kuchomwa moto kwa kuchomwa moto, jeraha kwa jeraha, na pigo kwa pigo. “Mtu akimpiga jicho mtumwa wake wa kiume au wa kike na kuliharibu jicho lake, ni lazima amwachilie aende huru bila malipo kwa ajili ya jicho lake. Hali kadhalika, akimpiga hata kumngoa jino mtumwa wake wa kiume au wa kike, ni lazima amwachilie huru kwa ajili ya jino lake. “Ngombe akimpiga mtu pembe na kumwua, ng'ombe huyo atauawa kwa kupigwa mawe na nyama yake haitaliwa. Mwenye ng'ombe huyo hatakuwa na lawama. Lakini kama ng'ombe huyo amezoea kupiga watu pembe, na mwenyewe akaonywa lakini hakumfunga, kama ng'ombe huyo akiua mtu lazima apigwe mawe, na mwenyewe lazima auawe. Hata hivyo, huyo mtu akitozwa faini ili kuyaokoa maisha yake, ni lazima alipe kiasi kamili atakachotozwa. Ngombe akimpiga pembe mtoto wa mtu mwingine, shauri hili litaamuliwa kwa njia hiyohiyo. Kama ng'ombe huyo akimpiga pembe mtumwa wa kiume au wa kike, mwenye ng'ombe atamlipa bwana wa huyo mtumwa fedha zenye thamani ya shekeli thelathini, na huyo ng'ombe lazima auawe kwa kupigwa mawe. “Mtu akiacha shimo wazi, ama akichimba shimo kisha asilifunike, halafu ng'ombe au punda akatumbukia humo, huyo mwenye shimo hilo lazima atoe fidia; atamlipa mwenye mnyama huyo fedha, na mnyama aliyekufa atakuwa wake. “Ngombe wa mtu akimwumiza ng'ombe wa mtu mwingine na kumwua, basi, watu watamwuza huyo ng'ombe aliyebaki hai na kugawana bei yake; vilevile watagawana yule ng'ombe aliyekufa. Lakini kama huyo ng'ombe alikuwa amezoea kupiga wengine pembe na mwenyewe hakumfunga, mwenyewe atalipa ng'ombe kwa ng'ombe, na yule aliyeuawa atakuwa wake. “Mtu akiiba ng'ombe au kondoo na kumchinja au kumwuza, atatozwa ng'ombe watano kwa kila ng'ombe, na kondoo wanne kwa kila kondoo. Mwizi akipatikana anavunja nyumba, akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya mauaji. Lakini mwizi huyo akishikwa wakati jua limechomoza na kuuawa, aliyemuua atakuwa na hatia. Huyo mwizi anapaswa kulipa. Ikiwa hana kitu cha kulipa, basi, yeye mwenyewe atauzwa ili kulipia wizi wake. Kama mnyama aliyeibiwa atapatikana kwa huyo mwizi akiwa hai, basi, mwizi atalipa mara mbili, awe ni ng'ombe, punda au kondoo. “Mtu akiwalisha wanyama wake katika shamba la mizabibu au kumwachia mnyama wake kula katika shamba la mtu mwingine, atalipa hasara hiyo kwa mazao bora ya shamba lake mwenyewe au shamba lake la mizabibu. “Mtu akiwasha moto nao ukachoma miti ya miiba na kusambaa hadi kuteketeza miganda ya nafaka, au nafaka ya mtu mwingine ambayo bado haijavunwa, au shamba lote likateketea, aliyewasha moto huo lazima alipe hasara hiyo yote. “Mtu akimwachia mwenzake fedha au mali nyingine amtunzie, kisha ikaibiwa nyumbani mwake, mwizi akipatikana lazima alipe thamani yake mara mbili. Lakini mwizi asipopatikana, mwenye nyumba atakaribia mbele za Mungu ili kuthibitisha kwamba hakuhusika na wizi wa mali ya mwenzake. “Pakiwa na ubishi juu ya ng'ombe, au punda, au kondoo, au mavazi, au kitu chochote kilichopotea ambacho kila mmoja anadai ni chake, wanaohusika wataletwa mbele za Mungu. Yule ambaye Mungu ataamua amekosa, atamlipa mwenzake mara mbili. “Mtu akimkabidhi mwenzake punda, ng'ombe, kondoo au mnyama mwingine yeyote amtunzie, na mnyama huyo akafa au akaumia au akachukuliwa bila mtu yeyote kushuhudia, kiapo mbele ya Mwenyezi-Mungu kitaamua kati yao, kuonesha kwamba huyo aliyekabidhiwa hakuhusika na wizi wa mali ya mwenzake. Mwenye mnyama huyo atakubali hicho kiapo, na huyo mwenzake hatalipa malipo yoyote. Lakini kama aliibiwa kwake, ni lazima amlipe mwenyewe. Kama huyo mnyama aliraruliwa na wanyama wa porini, huyo mtu aliyekuwa amekabidhiwa lazima amlete kama ushahidi. Hatalipa malipo yoyote kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama wa porini. “Mtu akiazima mnyama kwa mwenzake, kisha mnyama huyo akaumia au akafa wakati mwenyewe hayuko, aliyeazima mnyama huyo ni lazima alipe kikamilifu. Lakini kama mwenyewe alikuwako, basi aliyemwazima hatalipa chochote. Kama alikuwa ni mnyama aliyekodishwa, mwenyewe ataikubali tu bei ya kukodisha. “Mtu akimshawishi bikira ambaye hajaposwa, akalala naye, lazima atoe mahari na kumwoa msichana huyo. Baba wa huyo msichana akikataa katakata kumwoza binti yake, mtu huyo atalipa fedha ya mahari inayostahili msichana aliye bikira. “Usimwache mwanamke mchawi aishi. “Anayezini na mnyama lazima auawe. “Anayemtolea tambiko mungu mwingine badala ya Mwenyezi-Mungu pekee, lazima aangamizwe kabisa. “Msimdhulumu mgeni wala kumtesa, maana nanyi pia mlikuwa wageni nchini Misri. Msimtese mjane au yatima. Kama mkiwadhulumu hao nao wakanililia, hakika nitakisikiliza kilio chao, na hasira yangu itawaka, nami nitawaueni kwa upanga, na wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu yatima. “Ukimkopesha fedha mtu yeyote miongoni mwa watu wangu walio maskini, usiwe kwake kama mdai, wala usimtoze riba. Ukilichukua vazi la mwenzako kuliweka rehani, lazima umrudishie kabla ya jua kutua, kwa kuwa hiyo ndiyo nguo yake ya pekee; ndiyo atakayojifunika nayo. Au wadhani atalalia nini? Akinililia nitamsikiliza, maana mimi ni mwenye huruma. “Usimtukane Mungu, wala kumlaani mkuu wa watu wako. “Usikawie kunitolea sehemu yangu kutokana na wingi wa mazao yako na divai yako. Mtanipa wazaliwa wenu wa kwanza wa kiume. Mtafanya vivyo hivyo kuhusu wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na kondoo wenu. Mtamwacha kila mzaliwa wa kwanza na mama yake kwa siku saba, na siku ya nane mtanitolea. Nyinyi mtakuwa watu waliowekwa wakfu kwangu. Kwa hiyo hamtakula nyama ya mnyama aliyeuawa na mnyama wa porini. Nyama hiyo mtawatupia mbwa. “Usitoe habari za uongo. Usishirikiane na mtu mwovu ili kuwa shahidi mbaya. Usifuate genge la watu kutenda uovu, wala usijumuike na genge la watu kutoa ushahidi mahakamani ili kupotosha haki. Usiwe na upendeleo katika kesi ya maskini. “Ukimkuta ng'ombe au punda wa adui yako amepotea, utamrudishia mwenyewe. Ukimwona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, msaidie mtu huyo kumsimamisha punda wake, wala usimwache na kwenda zako. “Usiipotoshe haki anayostahili maskini katika kesi yake. Jitenge mbali na mashtaka ya uongo wala usiwaue wasio na hatia na waadilifu, maana mimi sitamsamehe mtu mwovu. Usipokee rushwa, maana rushwa huwapofusha wakuu na kupotosha mambo ya wenye haki. “Usimdhulumu mgeni; nyinyi mwajua hali ya kuwa mgeni, maana mlikuwa wageni nchini Misri. “Kwa muda wa miaka sita utapanda mashamba yako na kuvuna mazao yake. Lakini mnamo mwaka wa saba, utayaacha mashamba yako bila kupanda mbegu, ili maskini miongoni mwa watu wako wapate chakula kilichosalia humo, na wanyama wa porini wale. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni. “Kwa siku sita utafanya kazi zako, lakini siku ya saba utapumzika, ili ng'ombe wako na punda wako pia wapate kupumzika; na watumwa wako na watumishi wa kigeni wapate kustarehe. Yazingatie yote niliyokuambia. Usiyataje hata kidogo majina ya miungu mingine; hayo yasisikike kinywani mwako. “Mara tatu kila mwaka mtafanya sikukuu kwa heshima yangu. Mtaadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu: Kama nilivyowaagiza, mtakula mikate isiyotiwa chachu kwa siku saba wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kwa sababu katika mwezi huo mlitoka Misri. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu. Mtaadhimisha sikukuu ya mavuno ya kwanza ya kazi zenu na ya mavuno ya mashamba yenu. Mtaadhimisha sikukuu ya kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka mnapokusanya mazao ya kazi zenu. Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele zangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu. “Usinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala usiyaache mafuta ya sikukuu yangu yabaki mpaka asubuhi. “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. “Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake. “Tazameni, mimi namtuma malaika awatangulie safarini ili awalinde na kuwafikisha katika nchi niliyowatayarishia. Msikilizeni na kutii atakachosema, wala msimwasi, kwani hatawasamehe uasi wenu maana nimemtuma kwa jina langu. Lakini mkimsikiliza kwa makini na kufanya yote asemayo, mimi nitakuwa adui wa adui zenu na mpinzani wa wapinzani wenu. Malaika wangu atakapowaongoza na kuwafikisha katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nikawaangamiza hao wote, msiiname mbele ya miungu yao kuiabudu, wala kuitumikia, wala msiige mambo yao. Bali mtawaangamiza kabisa na kuzivunjavunja nguzo zao. Mtanitumikia mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nami nitawabariki kwa chakula na maji na kuyaondoa magonjwa kati yenu. Hakutakuwa na mwanamke yeyote atakayepoteza mimba wala kuwa tasa katika nchi yenu. Nami nitawajalia maisha marefu. “Nitapeleka kitisho mbele yenu na kuwavuruga watu wote mtakaowakabili, na adui zenu nitawafanya wageuke na kuwakimbia. Nitapeleka manyigu mbele yenu ambao watawafukuza Wahivi, Wakanaani na Wahiti. Sitawaondoa watu hao katika mwaka mmoja, nchi isije ikabaki tupu na wanyama wa porini wakaongezeka mno na kuwazidi nguvu. Lakini nitawaondoa kidogokidogo mpaka hapo mtakapoongezeka na kuimiliki nchi hiyo. Mipaka ya nchi yenu itakuwa kutoka bahari ya Shamu hadi bahari ya Mediteranea, na kutoka jangwani mpaka mto Eufrate, maana nitawatia wakazi wa nchi hiyo mikononi mwenu, nanyi mtawafukuza wawaondoke. Msifanye agano lolote nao, wala na miungu yao. Msiwaruhusu waishi nchini mwenu wasije wakawafanya mtende dhambi dhidi yangu; maana kama mkiitumikia miungu yao, hakika hiyo itakuwa mtego wa kuwanasa.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Njoni kwangu, wewe Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli, mniabudu kwa mbali. Wewe Mose peke yako ndiwe utakayenikaribia, lakini wengine wasije karibu, na Waisraeli wasipande mlimani pamoja nawe.” Basi, Mose akaenda na kuwaambia watu wote maneno na maagizo yote Mwenyezi-Mungu aliyomwambia. Watu wote wakajibu kwa sauti moja, “Mambo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya.” Mose akayaandika maagizo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimpa. Kisha akaamka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili kulingana na idadi ya makabila kumi na mbili ya Israeli. Kisha akawatuma vijana wa Waisraeli wamtolee Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa na kumchinjia sadaka za amani za ng'ombe. Mose akachota nusu ya damu ya wanyama hao na kuiweka katika mabirika, na nusu nyingine akairashia ile madhabahu. Kisha akachukua kitabu cha agano la Mwenyezi-Mungu, akakisoma mbele ya watu, nao wakasema, “Hayo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya, nasi tutakuwa watiifu.” Mose akaichukua ile damu na kuwanyunyizia watu, akisema, “Hii ndiyo damu ya agano ambalo Mwenyezi-Mungu amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.” Kisha Mose, Aroni, Nadabu na Abihu na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya johari ya rangi ya samawati, kikiwa safi kama mbingu angavu. Na Mungu hakuwadhuru hao viongozi wa watu wa Israeli. Walimwona Mungu, wakala na kunywa. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Njoo kwangu juu mlimani, ungoje huko. Mimi nitakupa vibao viwili vya mawe vyenye sheria na amri nilizoandika kwa ajili ya kuwafunza Waisraeli.” Basi, Mose akaondoka pamoja na Yoshua, mtumishi wake, akaenda kwenye mlima wa Mungu. Mose aliwaambia wale wazee, “Tungojeni hapa mpaka tutakapowarudia. Aroni na Huri wako pamoja nanyi; yeyote aliye na tatizo na awaendee wao.” Basi, Mose akaenda mlimani, na wingu likaufunika mlima. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatua juu ya mlima Sinai na wingu likaufunika mlima kwa muda wa siku sita. Siku ya saba Mungu akamwita Mose kutoka katikati ya lile wingu. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulionekana mbele ya macho ya watu wa Israeli kama moto unaowaka juu ya mlima. Mose akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani. Alikaa huko kwa muda wa siku arubaini, mchana na usiku. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli wanipe michango ya matoleo, nawe upokee kwa niaba yangu. Utapokea kutoka kwa mtu yeyote atakayetoa kwa moyo mkunjufu. Utapokea matoleo yafuatayo: Dhahabu, fedha, shaba, sufu ya buluu, ya zambarau na nyekundu, kitani safi iliyosokotwa manyoya ya mbuzi; ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, ngozi za mbuzi, mbao za mjohoro, mafuta kwa ajili ya taa, viungo kwa ajili ya mafuta ya kuweka wakfu na kwa ajili ya ubani wenye harufu nzuri, vito vya sardoniki, na vito vingine kwa ajili ya mapambo ya kizibao cha kuhani na kifuko cha kifuani. Vilevile Waisraeli watanitengenezea hema takatifu, ili niweze kukaa kati yao. Utatengeneza hema hiyo na vifaa vyake kulingana na mfano nitakaokuonesha. “Waisraeli watengeneze sanduku la mbao za mjohoro, lenye urefu wa sentimita 110, upana sentimita 66, na kimo sentimita 66. Utalipaka sanduku hilo dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu pande zote. Kisha utalitengenezea pete nne na kuzitia miguuni pake, kila mguu pete moja. Utatengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka dhahabu. Mipiko hiyo utaipitisha katika pete zilizo pande mbili za sanduku, kwa ajili ya kulibebea. Mipiko hiyo itabaki daima katika pete; isitolewe wakati wowote. Ndani ya sanduku hilo utaweka vibao viwili vya mawe vya ushuhuda. “Kisha utatengeneza kwa dhahabu safi kiti cha rehema, urefu wake sentimita 110, na upana wake sentimita 66. Utatengeneza pia mfano wa viumbe hai viwili kwa kufua dhahabu, uviweke kwenye miisho miwili ya kiti hicho; kiumbe kimoja mwisho mmoja na kiumbe kingine mwisho mwingine. Viweke viumbe hivyo kwenye miisho ya kiti hicho, lakini viwe kitu kimoja na hicho kiti. Viumbe hivyo vitaelekeana, mabawa yake yamekunjuka kukifunika kiti cha rehema; nyuso zake zitaelekea kiti hicho. Ndani ya sanduku utaweka vibao viwili vya mawe na kukiweka kiti cha rehema juu yake. Mimi nitakutana nawe hapo; na kutoka juu ya kiti hicho cha rehema katikati ya viumbe hao walioko juu ya sanduku la ushuhuda, nitazungumza nawe na kukupa amri zote kwa ajili ya Waisraeli. “Utatengeneza meza ya mbao za mjohoro yenye urefu wa sentimita 88, upana sentimita 44 na kimo sentimita 66. Hiyo meza utaipaka dhahabu safi na kuizungushia utepe wa dhahabu. Kisha utaizungushia ubao wenye upana wa sentimita 66. Utaitengenezea pete nne za dhahabu na kuzitia kwenye pembe zake miguuni pake. Pete hizo zitakuwa karibu na ule ubao wa kuizunguka meza na zitakuwa za kushikilia mipiko ya kuibebea hiyo meza. Utatengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka dhahabu; mipiko itakuwa ya kuibebea hiyo meza. Utatengeneza sahani na vikombe vya kuwekea ubani mezani, na pia bilauri na bakuli za kumiminia tambiko za kinywaji. Vifanye vyombo hivyo vyote kwa dhahabu safi. Meza hiyo utaiweka mbele ya sanduku la agano, na juu ya meza hiyo utaiweka ile mikate ya kuwekwa mbele yangu daima. “Utatengeneza kinara cha taa kwa dhahabu safi. Tako lake na ufito wa hicho kinara vitakuwa kitu kimoja, kadhalika na vikombe vyake, matumba yake na maua yake, vyote vitafuliwa kwa kipande kimoja tu cha dhahabu. Matawi sita yatatokeza kila upande wa ufito wake, matawi matatu upande mmoja na matawi matatu upande mwingine. Katika kila tawi kutakuwa na vikombe vitatu mfano wa maua ya mlozi, kila kimoja na tumba lake na ua lake. Na katika ufito kutakuwa na vikombe vinne mfano wa maua ya mlozi, pamoja na vifundo vyake na maua yake. Mahali panapotokezea kila jozi ya matawi yale sita, chini yake patakuwa na kifundo kimojakimoja. Vifundo hivyo na matawi yake yatakuwa kitu kimoja na kinara hicho, na chote kitafuliwa kwa dhahabu safi. Utatengeneza pia taa saba kwa ajili ya kinara hicho na kuziweka juu yake ili ziangaze kwa mbele. Tengeneza pia koleo zake na visahani vyake kwa dhahabu safi. Utatumia kilo thelathini na tano za dhahabu safi kutengeneza kinara hicho na vifaa vyake. Hakikisha kwamba umevitengeneza kwa mfano uliooneshwa kule mlimani. “Zaidi ya hayo yote, utatengeneza hema takatifu kwa mapazia kumi ya kitani safi iliyosokotwa, na kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu. Mapazia hayo utayapamba kwa michoro ya viumbe wenye mabawa waliotariziwa. Kila pazia litakuwa na urefu wa mita 12 na upana wa mita 2. Mapazia hayo yawe ya kipimo kimoja. Utaunganisha mapazia matano yawe kipande kimoja na mapazia mengine matano yawe kipande cha pili. Utashonea vitanzi vya buluu upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, hali kadhalika utashonea vitanzi mwishoni mwa pindo la nje la kipande kingine cha pazia. Utatia vitanzi hamsini katika pazia moja na vitanzi vingine hamsini kwenye utepe wa pazia la pili; vitanzi vyote vielekeane. Kisha utatengeneza kulabu hamsini za dhahabu ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia, hivyo hema litakuwa kitu kimoja. “Pia utatengeneza kifuniko cha hema kwa mapazia kumi na moja ya manyoya ya mbuzi. Kila pazia litakuwa na urefu wa mita 13, na upana wa mita 2. Mapazia yote hayo 11 yatakuwa na kipimo kilekile. Utaunga mapazia matano pamoja, na mapazia sita pamoja. Pazia la sita utalikunja mara mbili mbele ya hema. Kisha utafanya vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha pili. Utatengeneza kulabu hamsini za shaba na kuziingiza katika vile vitanzi hamsini ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia na hivyo kufanya pazia moja la hema. Ile nusu ya pazia iliyobaki utaitundika upande wa nyuma wa hema. Nusu mita ya urefu wa mapazia iliyo ya ziada utaikunja ininginie pande zote mbavuni mwa hema ili kulifunika. Utatengeneza pia kifuniko kingine cha hema kilichofanywa kwa ngozi laini ya kondoo dume na ngozi laini ya mbuzi. “Utatengeneza mbao za mjohoro za kusimama wima kwa ajili ya hema. Kila ubao utakuwa na urefu wa mita 4, na upana wa sentimita 66. Kila ubao utakuwa na ndimi mbili za kuunganishia. Utazifanyia mbao zote ndimi mbili. Basi, utatengeneza hizo mbao za hema hivi: Mbao ishirini kwa ajili ya upande wa kusini, na vikalio arubaini vya fedha chini ya hizo mbao ishirini, vikalio viwili chini kwa kila ubao ili kushikilia zile ndimi zake mbili na vikalio viwili viwe chini ya ubao mwingine ili kushikilia zile ndimi zake mbili. Upande wa kaskazini wa hema, utatengeneza mbao ishirini, na vikalio vyake arubaini vya fedha, vikalio viwili chini ya kila ubao. Kwa upande wa nyuma, ulio magharibi ya hema, utatengeneza mbao sita. Utatengeneza pia mbao mbili kwa ajili ya pembe za hema upande wake wa nyuma. Mbao hizo za pembeni ziachane chini lakini zishikamanishwe kwa juu kwenye pete ya kwanza. Mbao zote za pembeni zifanywe vivyo hivyo ili zifanye pembe mbili. Hivyo kutakuwa na mbao nane pamoja na vikalio vyake kumi na sita vya fedha: Vikalio viwili chini ya kila mbao na vikalio viwili chini ya ubao mwingine. “Utatengeneza pau za mjohoro; pau tano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa hema, na pau tano kwa ajili ya upande wa pili wa hema, na pau tano kwa ajili ya mbao za upande wa nyuma wa hema, ulio magharibi. Upau wa katikati uliofika nusu ya jengo la hema utapenya katikati toka mwisho huu hadi mwisho mwingine wa hema. Mbao zote utazipaka dhahabu na kuzifanyia pete za dhahabu zitakazoshikilia hizo pau, ambazo pia utazipaka dhahabu. Hivyo utalitengeneza hema hilo kulingana na mfano niliokuonesha mlimani. “Utatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Pazia hilo utalitarizi kwa ustadi kwa viumbe wenye mabawa. Utalitundika pazia kwenye nguzo nne za mjohoro zilizopakwa dhahabu, zenye kulabu za dhahabu na vikalio vinne vya fedha. Utalitundika pazia hilo kwenye vifungo, kisha ulilete lile sanduku la ushuhuda humo ndani kukiwa na vibao viwili vya mawe, nyuma ya pazia hilo. Pazia hilo litatenga mahali patakatifu na mahali patakatifu sana. Ndani ya mahali patakatifu utakiweka kile kiti cha rehema juu ya sanduku la maamuzi. Ile meza ya mjohoro utaiweka upande wa nje wa pazia hilo, na kile kinara cha taa utakiweka upande wa kusini wa hema, mkabala wa meza. Meza hiyo itakuwa upande wa kaskazini. “Kwa ajili ya mlango wa hema utatengeneza pazia zito kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri. Vilevile utatengeneza nguzo tano za mjohoro na kuzipaka dhahabu. Nguzo hizo zitakuwa na kulabu za dhahabu, na kila moja itakuwa na tako la shaba. “Utatengeneza madhabahu kwa mbao za mjohoro. Madhabahu hiyo itakuwa ya mraba, urefu wake mita mbili na robo, na upana wake mita mbili na robo; kimo chake kitakuwa mita moja na robo. Katika kila pembe ya madhabahu hiyo utatengeneza upembe ambao utakuwa umeundwa kutokana na madhabahu yenyewe. Madhabahu hiyo yote utaipaka shaba. Utaitengenezea vyombo vyake: Vyungu vya majivu, sepetu, na mabirika, na nyuma na visahani vya kuchukulia moto. Vyombo vyake vyote utavitengeneza kwa shaba. Kisha utatengeneza wavu wa shaba wenye pete nne za shaba kwenye pembe zake nne. Wavu huo utauweka kwenye ukingo wa madhabahu upande wa chini ili ufike katikati ya madhabahu. Utatengeneza pia mipiko ya mjohoro ya kuibebea madhabahu; nayo utaipaka shaba. Mipiko hiyo itaingizwa kwenye zile pete kila upande wa madhabahu, wakati wa kuibeba. Utaitengeneza madhabahu kwa mbao, na iwe yenye mvungu ndani, kulingana na mfano niliokuonesha mlimani. “Utatengeneza ua wa hema la mkutano. Upande wa kusini wa ua kutakuwa na vyandarua vilivyotengenezwa kwa kitani safi iliyosokotwa ambavyo vitakuwa na urefu wa mita 44 kwa upande mmoja. Vyandarua hivyo vitashikiliwa na nguzo ishirini za shaba zenye vikalio vya shaba. Lakini kulabu za nguzo hizo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha. Hali kadhalika upande wa kaskazini, urefu wa chandarua utakuwa mita 44, na nguzo zake 20 za shaba, lakini kulabu za nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha. Upande wa magharibi wa ua utakuwa na chandarua chenye urefu wa mita 22, na nguzo zake 10 na vikalio vyake 10. Upande wa mashariki kuliko na mlango, ua utakuwa na upana wa mita 22. Chandarua cha upande mmoja wa mlango kitakuwa na upana wa mita 6.5, pamoja na nguzo tatu na vikalio vyake vitatu. Vilevile katika upande wa pili wa mlango chandarua kitakuwa mita 6.5, pamoja na nguzo tatu na vikalio vyake vitatu. Mlango wenyewe wa ua utakuwa na pazia zito lenye urefu wa mita 9, lililotengenezwa kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri. Pazia hilo litashikiliwa na nguzo nne zenye vikalio vinne. Nguzo zote kuuzunguka ua zitashikamanishwa kwa fito za fedha, kulabu zake zitakuwa za fedha na vikalio vyake vitakuwa vya shaba. Ua huo utakuwa na urefu wa mita 44, upana wa mita 22, na kimo cha mita 2.25. Vyandarua vyake vitakuwa vya kitani safi na vikalio vyake vya shaba. Vyombo vyote vya hema takatifu vya matumizi ya kila aina, pamoja na vigingi vyote na hata vile vya ua vitakuwa vya shaba. “Utawaamuru Waisraeli wakuletee mafuta safi kwa ajili ya taa, kuwe na taa inayowaka daima. Hiyo itakuwa ndani ya hema la mkutano nje ya pazia hilo mbele ya sanduku la maamuzi na Aroni na wanawe wataitunza mbele yangu tangu jioni mpaka asubuhi. Agizo hili sharti lifuatwe daima na Waisraeli wote, kizazi hata kizazi. “Nawe Mose umlete kwangu Aroni ndugu yako, pamoja na wanawe: Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari utawateua miongoni mwa Waisraeli, ili wanitumikie kama makuhani. Utamshonea ndugu yako Aroni mavazi matakatifu ili apate kuonekana mwenye utukufu na mzuri. Waagize mafundi wote ambao nimewapa maarifa wamtengenezee Aroni mavazi ili awekwe wakfu kwa ajili ya kazi ya ukuhani. Waambie wamtengenezee vitu vifuatavyo: Kifuko cha kifuani, kizibao, kanzu, joho iliyonakshiwa, kilemba na mshipi. Aroni nduguyo na wanawe watayavaa ili wanitumikie kama makuhani. Hao mafundi watatumia sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na nyuzi za dhahabu na kitani safi iliyosokotwa. “Watakitengeneza kizibao cha kuhani kwa nyuzi za dhahabu na sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kukitarizi vizuri. Kitakuwa na kamba mbili za kukifungia mabegani zilizoshonewa kwenye ncha zake mbili. Mkanda wa kukishikia utatengenezwa kwa vifaa hivyohivyo: Kwa nyuzi za dhahabu, sufu ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa na kuwa kitu kimoja na kizibao hicho. “Kisha utachukua mawe mawili ya sardoniki ambayo utachora juu yake majina ya wana wa Israeli. Majina sita katika jiwe la kwanza, na majina sita yaliyobakia katika jiwe la pili; majina yafuatane kadiri ya kuzaliwa kwao. Utayachora majina hayo juu ya hayo mawe kama vile sonara achoravyo mhuri, kisha uyatie nakshi na kuyaingiza katika vijalizo vya dhahabu. Mawe hayo mawili yatawekwa juu ya kanda za kizibao kama kumbukumbu ya makabila kumi na mawili ya Israeli. Hivyo Aroni atavaa majina hayo mabegani mwake mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu kama ukumbusho. Utayatengenezea vijalizo viwili vya dhahabu, na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba. Utaifunga mikufu hiyo kwenye hivyo vijalizo. “Utatengeneza kifuko cha kifuani cha kauli cha maamuzi; kitengenezwe kwa ustadi sawa kama kilivyotengenezwa kile kizibao: Kwa dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa. Kifuko hicho ambacho kimekunjwa kitakuwa cha mraba, sentimita 22. Kitapambwa kwa safu nne za mawe ya thamani: Safu ya kwanza itakuwa ya akiki, topazi na almasi nyekundu; safu ya pili itakuwa ya zumaridi, johari ya rangi ya samawati na almasi; safu ya tatu itakuwa ya yasintho, akiki nyekundu na amethisto; na safu ya nne itakuwa ya zabarajadi, shohamu na yaspi; yote yatatiwa kwenye vijalizo vya dhahabu. Basi, patakuwa na mawe kumi na mawili yaliyochorwa majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. Kila moja litakuwa kama mhuri, ili kuwakilisha makabila yale kumi na mawili. Kwa ajili ya kifuko hicho cha kifuani, utatengeneza mikufu ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba. Vilevile utatengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya kifuko cha kifuani na kuzitia kwenye ncha mbili za kifuko hicho, na mikufu miwili ya dhahabu uifunge kwenye pete hizo za kifuko cha kifuani. Zile ncha mbili za mkufu wa dhahabu utazishikamanisha kwenye vile vijalizo viwili vya kile kibati ili zishikamane na kipande cha mabegani cha kizibao upande wa mbele. Pia utatengeneza pete mbili za dhahabu na kuzitia kwenye ncha mbili za chini upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kizibao. Kisha utatengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzitia mbele katika ncha za chini za vipande vya kizibao, mahali kizibao kinapoungana na mkanda uliofumwa kwa ustadi. Kifuko cha kifuani kitafungwa kwenye kizibao kwa kufunganisha pete zake na kizibao kwa kamba ya rangi ya buluu, ili kifuko hicho cha kifuani kisilegee ila kikalie ule mkanda uliofumwa kwa ustadi. “Aroni anapoingia mahali patakatifu, atavaa kifuko cha kauli kimechorwa majina ya makabila ya wana wa Israeli; kwa namna hiyo mimi Mwenyezi-Mungu sitawasahau nyinyi kamwe. Kwenye kifuko hicho utatia mawe ya kauli yaninginie kifuani mwa Aroni kila anapokuja mbele yangu. Nyakati hizo ni lazima kila mara kuvaa kifuko hicho, ili aweze kutambua matakwa yangu kuhusu Waisraeli. “Utashona kanzu ya kuvalia kizibao kwa sufu ya rangi ya buluu. Itakuwa na nafasi ya kupitishia kichwa katikati, na nafasi hiyo itazungushiwa utepe uliofumwa ili isichanike. Kwenye upindo wake wa chini, kuzunguka pande zote, itapambwa kwa makomamanga ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, kutakuwa pia na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga: Komamanga, njuga, komamanga, njuga, kuizunguka kanzu yote. Aroni atavaa kanzu hiyo kutekeleza huduma yake ya ukuhani na sauti yake itasikika wakati anapoingia mahali patakatifu mbele yangu na wakati anapotoka, njuga hizo zitasikika, naye hatauawa. “Kisha, utatengeneza kibati cha dhahabu safi na kuchora juu yake kama mtu achoravyo mhuri, ‘Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.’ Kibati hicho utakifunga mbele ya kilemba kwa ukanda wa buluu. Aroni atakivaa kibati hicho kwenye paji la uso wake; kwa hicho kibati atachukua lawama ya makosa ambayo Waisraeli wanaweza kuwa wameyafanya katika kunitolea tambiko takatifu, nami nitazikubali tambiko zao. Utamtengenezea Aroni joho iliyonakshiwa kwa kitani safi na kumfumia kilemba cha kitani safi na ukanda ulionakshiwa vizuri. “Utawatengenezea wana wa Aroni majoho, mishipi na kofia ili waonekane wana utukufu na uzuri. Utamvalisha ndugu yako Aroni na wanawe mavazi hayo, kisha uwapake mafuta na kuwawekea mikono ili kuwaweka wakfu wanitumikie kama makuhani. Vilevile utawashonea suruali za kitani zitakazowafunika tangu kiunoni mpaka mapajani, ili wafunike uchi wao. Aroni na wanawe watavaa suruali hizo kila wanapoingia katika hema la mkutano, au wanapokaribia kwenye madhabahu, kufanya huduma za makuhani katika mahali patakatifu. Kwa njia hiyo hawataonesha uchi wao na kuwa na hatari ya kuuawa. Hiyo itakuwa kanuni ya kudumu kwa Aroni na wazawa wake. “Haya ndiyo mambo utakayowafanyia Aroni na wanawe ili kuwaweka wakfu wanitumikie kama makuhani. Utachukua ndama dume na kondoo madume wawili wasio na dosari, mikate isiyotiwa chachu, maandazi yasiyotiwa chachu yaliyokandwa kwa mafuta, na mikate myembamba isiyotiwa chachu, lakini iliyopakwa mafuta. Vyote hivi viwe vimetengenezwa kwa unga laini wa ngano. Kisha iweke hiyo mikate ndani ya kikapu kimoja na kunitolea wakati mmoja na yule ndama dume na wale kondoo dume wawili. “Kisha wapeleke Aroni na wanawe mlangoni pa hema la mkutano na kuwatawadha. Kisha utachukua yale mavazi ya kikuhani umvike Aroni: Joho, kanzu, kizibao, kifuko cha kifuani, na kumfunga ule mshipi uliofumwa kwa ustadi. Tena utamvika kile kilemba kichwani na kuweka juu ya hicho kilemba ile taji takatifu. Baada ya kufanya hivyo, utachukua yale mafuta ya kupaka, ummiminie Aroni kichwani mwake kumweka wakfu. “Kisha utawaleta wana wa Aroni na kuwavika vizibao. Utawafunga mishipi viunoni na kuwavisha kofia zao. Hivyo ndivyo utakavyowaweka wakfu Aroni na wanawe kuwa makuhani. Hao watakuwa makuhani daima. “Kisha utamleta yule ndama dume mbele ya hema la mkutano. Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha ndama huyo na kumchinja mbele ya Mwenyezi-Mungu, mlangoni pa hema la mkutano. Utachukua kiasi cha damu na kuipaka kwenye pembe za madhabahu kwa kidole chako, na damu yote inayosalia utaimwaga chini ya madhabahu. Halafu utatwaa mafuta yote yanayofunika matumbo, sehemu bora ya maini pamoja na figo mbili na mafuta yake, uviteketeze vyote juu ya madhabahu. Lakini nyama ya fahali huyo pamoja na ngozi na mavi yake utavichukua na kuviteketeza nje ya kambi yenu. Hii itakuwa sadaka ya kuondoa dhambi. “Kisha utamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumwambia Aroni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake. Nawe utamchinja na damu yake utairashia madhabahu pande zake zote. Halafu utamkata huyo kondoo vipandevipande; utaosha matumbo yake na miguu yake, uviweke vyote pamoja na kichwa na vipande vingine. Kisha utamteketeza kondoo mzima juu ya madhabahu ili kunitolea sadaka ya kuteketezwa; harufu ya sadaka inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. “Utamchukua yule kondoo mwingine, naye Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. Nawe utamchinja na kuchukua kiasi cha damu na kumpaka Aroni na wanawe kwenye ncha za masikio yao ya kulia na vidole gumba vya mikono yao ya kulia, na vidole gumba vya miguu yao ya kulia. Damu inayobaki utairashia madhabahu pande zake zote. Kisha utachukua kiasi cha damu iliyoko juu ya madhabahu pamoja na yale mafuta ya kupaka umnyunyizie Aroni na mavazi yake, uwanyunyizie pia wanawe na mavazi yao. Aroni na wanawe watakuwa wamewekwa wakfu kwangu pamoja na mavazi yao yote. “Kisha utachukua mafuta ya huyo kondoo dume: Mkia wake, mafuta yanayofunika matumbo na sehemu bora ya maini, figo zake mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Kondoo huyo ni kondoo wa kuweka wakfu.) Kutoka katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu kilicho mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu, utachukua mkate mmoja na andazi moja lililotiwa mafuta na mkate mwembamba mmoja. Vyote hivi utamkabidhi Aroni na wanawe nao wataviinua juu kuwa ishara ya kunitolea tambiko mimi Mwenyezi-Mungu. Kisha utavichukua tena kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu pamoja na ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri itakayonipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. Hiyo ni sadaka inayotolewa kwa moto. “Kisha utachukua kidari cha huyo kondoo wa kumweka wakfu Aroni, na kufanya ishara ya kunitolea mimi Mwenyezi-Mungu. Nacho kitakuwa sehemu yako. Kuhani anapowekwa wakfu, kidari na paja la kondoo dume wa kuwekea wakfu vitaletwa na kuwekwa wakfu mbele yangu kwa kufanya ishara ya kunitolea, navyo vitakuwa vya Aroni na wanawe. Hivyo Waisraeli daima watachukua sehemu hizo kutoka katika sadaka zao za amani wanazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu na kumpa Aroni na wanawe. Hiyo ni sadaka yao kwa Mwenyezi-Mungu. “Baada ya kufa kwake Aroni, mavazi yake matakatifu yatakabidhiwa wazawa wake, nao watayavaa siku yao ya kupakwa mafuta na kuwekewa mikono. Mwana wa Aroni atakayekuwa kuhani mahali pa baba yake atayavaa mavazi hayo siku saba katika hema la mkutano, ili kuhudumu katika mahali patakatifu. “Utachukua nyama ya huyo kondoo wa kuwaweka wakfu na kuichemshia katika mahali patakatifu. Kisha utawapa Aroni na wanawe, nao wataila mlangoni pa hema la mkutano pamoja na ile mikate iliyosalia kapuni. Watavila vitu hivyo vilivyotumika kuwaweka wakfu na kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho, lakini mtu mwingine asiruhusiwe kuvila kwani ni vitakatifu. Kama nyama yoyote au mikate hiyo itasalia mpaka asubuhi yake, basi utaiteketeza kwa moto; isiliwe maana ni kitu kitakatifu. “Hivyo ndivyo utakavyowatendea Aroni na wanawe kufuatana na yote yale niliyokuamuru; utawaweka wakfu kwa muda wa siku saba, na kila siku utatoa fahali awe sadaka ya kuondolea dhambi ili kufanya upatanisho, na kwa kufanya hivyo utaitakasa madhabahu; kisha utaimiminia mafuta ili kuiweka wakfu. Kwa siku saba utaifanyia madhabahu upatanisho na kuiweka wakfu. Baada ya hayo, madhabahu itakuwa takatifu kabisa na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu. “Kila siku, wakati wote ujao, utatolea sadaka juu ya madhabahu: Wanakondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja. Mwanakondoo mmoja utamtoa sadaka asubuhi na mwingine jioni. Pamoja na mwanakondoo wa kwanza, utatoa kilo moja ya unga laini uliochanganywa na lita moja ya mafuta safi, na lita moja ya divai kama sadaka ya kinywaji. Hali kadhalika na yule mwanakondoo mwingine wa jioni utamtolea tambiko pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji kama ulivyofanya asubuhi; harufu ya tambiko hiyo inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. Sadaka hii ya kuteketezwa itatolewa daima, kizazi hata kizazi, mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu, mbele ya mlango wa hema la mkutano ambapo mimi nitakutana nanyi na kuongea nanyi. Hapo ndipo nitakapokutana na Waisraeli na utukufu wangu utapafanya pawe patakatifu. Hema la mkutano na madhabahu nitavifanya vitakatifu; vilevile Aroni na wanawe nitawaweka wakfu ili wanitumikie kama makuhani. Nitaishi kati ya Waisraeli, nami nitakuwa Mungu wao. Hapo ndipo watakapotambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili niishi kati yao. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. “Utatengeneza madhabahu kwa mbao za mjohoro ili pawe mahali pa kufukizia ubani. Madhabahu hiyo iwe ya mraba, urefu na upana wake sentimita 45, na kimo chake sentimita 90. Pembe zake za juu zitatokeza zote zikiwa kitu kimoja na madhabahu yenyewe. Yote utaipaka dhahabu safi: Upande wake wa juu, pande zake zote za ubavuni na pembe zake; pia utaizungushia ukingo wa dhahabu. Utaitengenezea pete mbili za dhahabu na kuzitia chini ya ukingo wake kwenye pande mbili zinazokabiliana; hizo pete zitatumiwa kushikilia mipiko wakati wa kuibeba. Mipiko hiyo iwe ya mjohoro na ipakwe dhahabu. Madhabahu hiyo iwekwe mbele ya pazia kando ya sanduku la maamuzi, mbele ya kiti cha huruma ambapo nitakutana nawe. Kila siku Aroni anapoingia kuzitayarisha taa zilizopo hapo, atafukiza ubani wenye harufu nzuri juu ya madhabahu hiyo. Tena atafukiza ubani wakati wa jioni anapowasha taa. Tambiko hii ya ubani itatolewa daima bila kukatizwa katika vizazi vyenu vyote. Kwenye madhabahu hiyo, kamwe msifukize ubani usio mtakatifu, wala msitoe sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya nafaka, wala kumimina juu yake sadaka ya kinywaji. Aroni hana budi kufanya upatanisho juu ya pembe za madhabahu hiyo mara moja kwa mwaka. Ataifanyia upatanisho kwa damu ya tambiko ya kuondolea dhambi mara moja kila mwaka katika vizazi vyenu vyote maana madhabahu hiyo ni takatifu kabisa kwangu mimi Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kila utakapowahesabu Waisraeli, kila mmoja atalipa fidia kwa ajili ya nafsi yake mbele yangu ili pasiwe na maradhi mabaya miongoni mwao wakati wa kuhesabiwa. Kila mmoja atakayehesabiwa ni lazima alipe kiasi cha fedha kulingana na vipimo vya hema la mkutano. Hii ni sadaka yake atakayonitolea. Kila mmoja atakayehesabiwa, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, atanitolea tambiko hiyo. Tajiri asitoe zaidi wala maskini asitoe chini ya nusu ya kiasi hicho cha fedha wakati mnaponitolea sadaka hiyo ili kufanya upatanisho. Wewe utaipokea fedha hiyo ya upatanisho kutoka kwa Waisraeli, nawe utaitumia kwa shughuli za kazi za hema takatifu, nayo iwe ni ukumbusho wa Waisraeli mbele yangu, fidia ya maisha yenu.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utatengeneza birika la shaba la kutawadhia lenye tako la shaba, uliweke katikati ya hema la mkutano na madhabahu, na kutia maji ndani yake. Aroni na wanawe watatumia maji hayo kunawia mikono na miguu, kabla ya kuingia kwenye hema la mkutano au kukaribia madhabahu ili kunitolea tambiko mimi Mwenyezi-Mungu, tambiko zitolewazo kwa moto; watafanya hivyo wasije wakafa. Ni lazima wanawe mikono na miguu yao wasije wakafa. Hii itakuwa ni kanuni kwao daima, tangu Aroni na uzao wake, vizazi hata vizazi.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utachukua viungo bora kabisa kama vifuatavyo: Manemane ya maji kilo sita, mdalasini wenye harufu nzuri kilo tatu, miwa yenye harufu nzuri kilo tatu, na aina nyingine ya mdalasini kilo 6 — vipimo hivyo vyote viwe kufuatana na vipimo vya hema takatifu; chukua pia lita 4 za mafuta. Kutokana na viungo hivyo utatengeneza mafuta matakatifu uyachanganye kama afanyavyo fundi wa manukato; hayo yatatumika kuweka vitu wakfu. Kisha utalimiminia mafuta hayo hema la mkutano, na sanduku la maamuzi; meza na vyombo vyake vyote; kinara cha taa na vyombo vyake, madhabahu ya kufukizia ubani, madhabahu ya sadaka za kuteketezwa na vyombo vyake vyote, birika na tako lake. Utaviweka wakfu, ili viwe vitakatifu kabisa. Chochote kitakachovigusa vifaa hivyo, kitakuwa kitakatifu. Kisha mpake mafuta Aroni na wanawe na kuwaweka wakfu ili wanitumikie kama makuhani. Waambie Waisraeli kwamba haya yatakuwa mafuta yangu matakatifu ya kupaka katika vizazi vyenu vyote. Mafuta haya kamwe yasimiminiwe mtu yeyote wa kawaida, wala yasitengenezwe mafuta mengine ya aina hii; haya ni mafuta matakatifu na ni lazima yawe daima matakatifu kwenu. Yeyote atakayetengeneza mafuta kama haya, au kumpaka mtu asiyestahili kupakwa mafuta haya, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utachukua vipimo vinavyolingana vya viungo vitamu vifuatavyo: Utomvu wa natafi, utomvu wa shekelethi, utomvu wa kelbena na ubani safi. Utatumia vitu hivyo kutengenezea ubani kama utengenezwavyo na fundi manukato, utiwe chumvi upate kuwa safi na mtakatifu. Kisha utasagwa na kufanya unga laini, upate kutumiwa ndani ya hema la mkutano na kulipaka sanduku la agano, mahali nitakapokutana nawe; huo utakuwa ubani mtakatifu kabisa kwenu. Kamwe msifanye ubani wa mchanganyiko huo kwa matumizi yenu wenyewe kwani ubani huo utakuwa mtakatifu mbele yangu. Yeyote atakayejitengenezea ubani wa aina hiyo na kuutumia kama manukato yake binafsi, atatengwa mbali na watu wake.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mimi nimemteua Bezaleli, mwana wa Uri, mjukuu wa Huri, wa kabila la Yuda na kumjaza roho wangu. Nimempatia uzoefu na akili, maarifa na ufundi, ili abuni kazi za usanii na kufanya kazi za kufua dhahabu, fedha na shaba. Nimempatia ujuzi wa kuchonga mawe ya kupambia, kuchonga mbao, na ujuzi wa kila aina ya ufundi. Vilevile nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, afanye kazi pamoja naye. Hali kadhalika nimewapa uwezo mkubwa watu wengine kwa ajili ya kazi mbalimbali, ili watengeneze vifaa vyote nilivyoagiza vifanywe: Hema la mkutano, sanduku la ushuhuda na kiti cha ushuhuda juu yake, pamoja na vifaa vyake vyote; meza na vyombo vyake, kinara safi cha taa na vyombo vyake, madhabahu ya kufukizia ubani, madhabahu ya sadaka za kuteketezwa na vyombo vyake vyote, birika la maji pamoja na tako lake, mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na wanawe ambao watafanya huduma ya ukuhani, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri kwa ajili ya mahali patakatifu. Vitu hivyo vyote vitatengenezwa kulingana kabisa na jinsi nilivyokuamuru.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Nyinyi mtaadhimisha Sabato zangu, kwa sababu hizo ni ishara kati yenu na mimi kwa vizazi vyote kwamba mimi ndimi ninayewatakasa. Mtaiadhimisha Sabato, nayo itakuwa kwenu siku takatifu. Yeyote atakayeitia unajisi siku hiyo lazima auawe. Na mtu atakayefanya kazi yoyote siku hiyo atatengwa mbali na watu wake. Mtafanya kazi zenu kwa muda wa siku sita, lakini siku ya saba ni siku rasmi ya mapumziko, ni siku yangu takatifu. Mtu yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo lazima atauawa. Kwa hiyo Waisraeli wataiadhimisha siku ya Sabato katika vizazi vyao vyote kama ishara ya agano la milele. Jambo hili litakuwa ishara ya kudumu kati ya Waisraeli na mimi, maana mimi Mwenyezi-Mungu nilifanya mbingu na dunia kwa muda wa siku sita, lakini siku ya saba niliacha kufanya kazi, nikapumzika.” Mwenyezi-Mungu alipomaliza kuongea na Mose mlimani Sinai, alimpatia Mose vile vibao viwili vya mawe ambavyo yeye Mungu aliviandika zile amri kwa kidole chake mwenyewe. Watu walipoona kuwa Mose amechelewa kurudi kutoka mlimani, walikusanyika mbele ya Aroni na kumwambia, “Haya! Tutengenezee miungu itakayotuongoza maana hatujui lililompata huyo Mose aliyetutoa nchini Misri.” Aroni akawajibu, “Chukueni vipuli vya dhahabu masikioni mwa wake zenu, wana wenu na binti zenu, mniletee.” Basi, watu wote wakatoa vipuli vyote vya dhahabu masikioni mwao, wakamletea Aroni. Naye akavichukua akaviyeyusha, akatengeneza ndama wa kusubu. Watu wakapaza sauti, “Ee Israeli, huyu ndiye mungu wetu aliyetutoa nchini Misri.” Kisha Aroni akamjengea huyo ndama madhabahu, halafu akatangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.” Kesho yake watu waliamka mapema wakatoa sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani. Watu wakaketi chini kula na kunywa; kisha wakasimama na kucheza. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Teremka chini kwa maana watu wako uliowaleta kutoka nchini Misri wamejipotosha wenyewe; wameiacha mara moja njia niliyowaamuru, wakajifanyia ndama wa kusubu, nao wamemwabudu na kumtolea tambiko wakisema, ‘Ee Israeli, huyu ndiye mungu wetu aliyetutoa nchini Misri!’ Nawafahamu watu hawa; wao wana vichwa vigumu. Sasa, usijaribu kunizuia. Niache niwaangamize kwa ghadhabu kali; kisha kutokana nawe nitaunda taifa kubwa.” Lakini Mose akamsihi Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, kwa nini hasira yako inawaka vikali dhidi ya watu wako uliowatoa nchini Misri kwa uwezo mkuu na mkono wenye nguvu? Ukifanya hivyo, hakika Wamisri watasema, ‘Aliwatoa kwa nia mbaya ili kuwaulia mlimani na kuwateketeza kabisa duniani.’ Ee Mwenyezi-Mungu, tuliza hasira yako kali na kuacha jambo hilo baya ulilokusudia kufanya dhidi ya watu wako. Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, Isaka na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe, ukisema, ‘Nitawazidisha wazawa wenu kama nyota za mbinguni na nchi yote hii niliyowaahidia nitawapa vizazi vyenu wairithi milele.’” Basi, Mwenyezi-Mungu akaacha kuwafanyia watu wake lile jambo baya alilokuwa amesema. Kisha Mose akashuka kutoka mlimani akiwa na vibao viwili vya mawe mikononi mwake, vimeandikwa amri za Mungu pande zote. Vibao hivyo vilikuwa kazi yake Mungu mwenyewe na maandishi hayo aliyachora Mungu mwenyewe. Yoshua aliposikia kelele za watu, akamwambia Mose, “Kuna kelele za vita kambini.” Lakini Mose akamjibu, “Si kelele ya ushindi au kushindwa, bali kelele ninayosikia ni kelele ya watu wanaoimba.” Mara tu walipoikaribia kambi walipomwona yule ndama na watu wakicheza; hapo hasira ya Mose ikawaka kama moto, akavitupa chini vile vibao kutoka mikononi mwake na kuvivunja pale chini ya mlima. Basi, akamchukua yule ndama akamchoma moto, akamsaga mpaka akawa unga, akaukoroga unga huo katika maji na kuwalazimisha Waisraeli wanywe. Mose akamwuliza Aroni, “Walikufanya nini watu hawa hata ukawaingiza katika dhambi kubwa hivyo?” Aroni akamjibu, “Nakuomba ee bwana wangu hasira yako isiniwakie mimi mtumishi wako. Unawafahamu jinsi watu hawa walivyo tayari kutenda maovu. Walikuja wakaniambia, ‘Tufanyie miungu ambayo itatuongoza kwani huyo Mose aliyetutoa nchini Misri hatujui lililompata’. Nami nikawaambia, kila mmoja aliye na vito vya dhahabu na avilete. Basi, wakaniletea, nami nikaviyeyusha motoni na huyu ndama akatokea.” Basi, Mose alipoona kuwa watu wameasi na kufanya wapendavyo (kwa kuwa Aroni aliwafanya waasi na kufanya wapendavyo, na kujiletea aibu mbele ya adui zao), Mose akasimama mbele ya lango la kambi na kuuliza, “Ni nani aliye upande wa Mwenyezi-Mungu? Na aje kwangu.” Wana wote wa Lawi wakakusanyika pamoja mbele yake. Akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Kila mtu na ajifunge upanga wake kiunoni, azunguke kila mahali kambini, kutoka lango moja hadi lingine, na kila mmoja amuue ndugu yake, rafiki yake na jirani yake.’” Wana wa Lawi wakafanya kama Mose alivyowaagiza. Siku hiyo waliuawa watu wapatao 3,000. Mose akasema, “Leo mmejiweka wakfu nyinyi wenyewe kumhudumia Mwenyezi-Mungu, kwa vile hamkusita hata kuwaua watoto wenu au ndugu zenu. Mungu awajalie baraka leo hii.” Kesho yake Mose akawaambia watu, “Mmetenda dhambi kubwa! Sasa nitamwendea Mwenyezi-Mungu juu mlimani; labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.” Hivyo Mose akarudi kwa Mwenyezi-Mungu, akamwambia, “Nasikitika! Watu hawa wametenda dhambi kubwa; wamejifanyia wenyewe miungu ya dhahabu. Lakini sasa, nakuomba uwasamehe dhambi yao. Ikiwa hutawasamehe, nakusihi unifute mimi katika kitabu chako ulichowaandika watu wako.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nitamfuta katika kitabu changu mtu yeyote aliyenitendea dhambi. Lakini sasa nenda ukawaongoze watu mpaka mahali nilipokuambia. Tazama, malaika wangu atakutangulia. Hata hivyo, siku nitakapowajia, nitawaadhibu kwa sababu ya dhambi yao.” Mwenyezi-Mungu akawapelekea watu ugonjwa wa tauni, kwa kuwa walimwomba Aroni awafanyie yule ndama wa dhahabu. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Anza safari uondoke hapa, wewe na watu hao uliowatoa nchini Misri, mwende katika nchi niliyomwapia Abrahamu, Isaka na Yakobo, nikisema, ‘Nitawapa wazawa wenu nchi hii’. Nitamtuma malaika awaongoze; nitawafukuza Wakaanani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Nendeni katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali. Lakini kwa sababu nyinyi ni wenye vichwa vigumu sitakwenda pamoja nanyi, nisije nikawaangamiza njiani.” Watu walilia waliposikia habari hizi mbaya; wala hakuna aliyevaa mapambo yake. Walifanya hivyo kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘Nyinyi ni watu wenye vichwa vigumu; nikienda pamoja nanyi kwa muda mfupi tu, nitawaangamiza. Hivyo vueni mapambo yenu ili nijue namna ya kuwatendea.’” Basi, Waisraeli waliyavua mapambo yao tangu walipoondoka mlimani Horebu. Mose alikuwa na desturi ya kulichukua lile hema na kulisimika nje ya kambi. Hema hilo alilipa jina, Hema la Mkutano. Mtu yeyote aliyetaka shauri kwa Mwenyezi-Mungu alikwenda kwenye hema la mkutano nje ya kambi. Kila mara Mose alipotoka kwenda kwenye hema hilo, kila mtu alisimama penye mlango wa hema lake na kumwangalia Mose mpaka alipoingia ndani ya hilo hema. Wakati Mose alipoingia ndani ya hilo hema, mnara wa wingu ulitua kwenye mlango wa hema, na Mwenyezi-Mungu akaongea naye. Watu wote walipouona ule mnara wa wingu umesimama mlangoni mwa hema, kila mmoja wao alisimama na kuabudu mlangoni mwa hema lake. Hivyo ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyokuwa akiongea na Mose uso kwa uso, kama mtu na rafiki yake. Kisha Mose alirudi tena kambini. Naye kijana Yoshua mwana wa Nuni ambaye alikuwa mtumishi wake hakuondoka hemani. Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama! Wewe waniambia, ‘Waongoze watu hawa,’ lakini hujanijulisha ni nani utakayemtuma anisaidie. Hata hivyo umesema kwamba unanijua kwa jina na pia kwamba nimepata fadhili mbele zako. Sasa basi, nakusihi, kama kweli nimepata fadhili mbele yako, nioneshe sasa njia zako, ili nipate kukujua na kupata fadhili mbele zako. Naomba ukumbuke pia kwamba taifa hili ni watu wako.” Mungu akasema, “Mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nawe, na nitakupa faraja.” Mose akasema, “Kama wewe binafsi hutakwenda pamoja nami, basi, usituondoe mahali hapa. Maana nitajuaje kuwa nimepata fadhili mbele zako, mimi na watu wako kama usipokwenda pamoja nasi? Ukienda pamoja nasi itatufanya mimi na watu wako kuwa watu wa pekee miongoni mwa watu wote duniani.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa kuwa umepata fadhili mbele yangu, nami nakujua kwa jina lako, jambo hilihili ulilolisema nitalifanya.” Mose akasema, “Nakusihi unioneshe utukufu wako.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Nitapita mbele yako na kukuonesha wema wangu wote nikilitangaza jina langu, ‘Mwenyezi-Mungu’. Mimi nitamrehemu yule ninayependa kumrehemu, na kumhurumia yule ninayependa kumhurumia. Lakini hutaweza kuniona uso maana hakuna mwanadamu yeyote atakayeniona na kuishi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kuna mahali karibu nami ambapo utasimama juu ya mwamba; na utukufu wangu utakapokuwa unapita, nitakutia katika pango mwambani na kukufunika kwa mkono wangu, mpaka nitakapokuwa nimepita. Halafu nitauondoa mkono wangu nawe utaniona nyuma, lakini uso wangu hutauona.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nami nitayaandika maneno yale yaliyokuwa katika vile vibao vya kwanza ulivyovivunja. Uwe tayari kesho asubuhi, uje kukutana nami mlimani Sinai. Mtu yeyote asije pamoja nawe, wala asionekane popote mlimani; wala kondoo au ng'ombe wasilishwe karibu yake.” Basi, Mose akachonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza. Akaondoka asubuhi na mapema, akapanda mlimani Sinai, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru, akiwa na vile vibao viwili vya mawe mikononi mwake. Mwenyezi-Mungu akashuka katika wingu, akasimama pamoja na Mose, akalitaja jina lake, “Mwenyezi-Mungu.” Kisha Mwenyezi-Mungu akapita mbele ya Mose akitangaza tena, “Mwenyezi-Mungu; mimi Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mwenye huruma na neema; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili na uaminifu. Mimi nawafadhili maelfu, nikiwasamehe uovu, makosa na dhambi; lakini kwa vyovyote vile sitaacha kumwadhibu mwenye hatia; nawapatiliza watoto na wajukuu uovu wa baba na babu zao, hata kizazi cha tatu na nne.” Mose akainama chini mara, akamwabudu Mungu. Kisha akasema, “Ee Bwana wangu, kwa vile umenijalia fadhili mbele zako, nakuomba uende pamoja nasi. Watu hawa ni wenye vichwa vigumu, lakini utusamehe uovu wetu na dhambi yetu, utupokee kama watu wako mwenyewe.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Sasa ninafanya agano na watu wako. Nitatenda maajabu mbele yao ambayo hayajapata kutendwa duniani kote, wala katika taifa lolote. Na watu wote mnaoishi kati yao wataona matendo yangu makuu. Maana nitafanya jambo la ajabu kwa ajili yako. “Shikeni amri ninazowapa leo. Nitawafukuza mbele yenu Waamori, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Jihadharini msije mkafanya agano na wakazi wa nchi mnayoiendea, maana hilo litakuwa mtego miongoni mwenu. Lakini mtazibomoa madhabahu zao na kuzivunja nguzo zao za ibada na sanamu zao za Ashera. Msiabudu mungu yeyote mwingine, maana mimi Mwenyezi-Mungu najulikana kwa jina: ‘Mwenye Wivu,’ mimi ni Mungu mwenye wivu. Msifanye mikataba yoyote na wakazi wa nchi hiyo, maana watakapoiabudu miungu yao ya uongo na kuitambikia, watawaalikeni, nanyi mtashawishiwa kula vyakula wanavyoitambikia miungu yao, nao wavulana wenu wakaoa binti zao, na hao binti wanaoabudu miungu yao, wakawashawishi wavulana wenu kufuata miungu yao. “Msijifanyie miungu ya uongo ya chuma. “Mtaiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kama nilivyowaamuru, kwa sababu katika mwezi huo wa Abibu mlitoka Misri. Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume ni wangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wako wote, wa ng'ombe na wa kondoo. Mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa kunitolea kondoo. Kama hutamkomboa utamvunja shingo. Watoto wenu wote wa kiume ambao ni wazaliwa wa kwanza mtawakomboa. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu. “Siku sita mtafanya kazi zenu, lakini siku ya saba mtapumzika, hata ikiwa ni wakati wa kulima au kuvuna. Mtaadhimisha sikukuu ya majuma mwanzoni mwa majira ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka. Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele yangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Nitayafukuza mataifa mengine mbele yenu na kuipanua mipaka yenu. Hakuna mtu yeyote atakayeitamani nchi yenu wakati mnapokusanyika kuniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu mara tatu kila mwaka. “Msinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na chachu; wala tambiko ya sikukuu ya Pasaka isibakizwe mpaka asubuhi. “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. “Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Andika maneno haya, maana kulingana na maneno haya, ninafanya agano nawe na watu wa Israeli.” Mose alikaa huko mlimani pamoja na Mwenyezi-Mungu siku arubaini, mchana na usiku; hakula chakula wala kunywa maji. Aliandika maneno yote ya agano na zile amri kumi. Mose alipokuwa anashuka mlimani Sinai akiwa na vile vibao viwili vyenye maneno ya agano mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa unangaa kwa sababu alikuwa ameongea na Mwenyezi-Mungu. Aroni na watu Waisraeli wote walipomwona waliogopa kumkaribia, kwani uso wake ulikuwa unangaa. Lakini Mose alimwita Aroni na viongozi wa jumuiya ya Waisraeli waende karibu naye, kisha akazungumza nao. Baadaye Waisraeli wote wakaja karibu naye, naye akawapa amri zote ambazo Mwenyezi-Mungu alimpa kule mlimani Sinai. Mose alipomaliza kuzungumza na watu aliufunika uso wake kwa kitambaa. Lakini ikawa kwamba kila mara Mose alipokwenda kuongea na Mwenyezi-Mungu katika hema la mkutano, alikiondoa kile kitambaa mpaka alipotoka nje. Na alipotoka nje aliwaambia Waisraeli mambo yote aliyoamriwa, nao Waisraeli waliuona uso wake unangaa. Ndipo Mose alipoufunika tena uso wake kwa kitambaa mpaka alipokwenda kuongea na Mwenyezi-Mungu. Mose alikusanya jumuiya yote ya Waisraeli, akawaambia, “Haya ndiyo mambo ambayo Mwenyezi-Mungu amewaamuru muyafanye: Kwa siku sita mtafanya kazi zenu; lakini siku ya saba ni Sabato siku ya mapumziko ambayo ni wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Yeyote atakayefanya kazi siku hiyo lazima auawe. Msiwashe hata moto katika makao yenu siku ya Sabato.” Mose aliiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Hili ndilo jambo ambalo Mwenyezi-Mungu amewaamuru mlifanye: Mtatoa katika mali zenu mchango wa kumpa Mwenyezi-Mungu. Kila mtu mwenye moyo mwema atamletea Mwenyezi-Mungu mchango: Dhahabu, fedha, shaba; sufu ya buluu, ya zambarau na nyekundu; kitani safi iliyosokotwa; manyoya ya mbuzi; ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, ngozi za mbuzi; mbao za mjohoro, mafuta kwa ajili ya taa, viungo kwa ajili ya mafuta ya kupaka na kwa ajili ya ubani wenye harufu nzuri; vito vya sardoniki na vito vingine kwa ajili ya mapambo ya kizibao na kifuko cha kifuani. “Kila mtu mwenye ujuzi wa kazi fulani miongoni mwenu atakuja kufanya vitu vyote alivyoamuru Mwenyezi-Mungu: Kutengeneza hema takatifu, kifuniko chake na pazia lake, kulabu zake, pau zake, vikalio vyake; sanduku la agano pamoja na mipiko yake, kiti cha rehema, pazia la mahali patakatifu sana; meza na mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; vinara vya taa pamoja na vyombo vyake vyote, taa zake na mafuta yake; madhabahu ya ubani na mipiko yake, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri, pazia la mlango wa hema takatifu; madhabahu ya sadaka za kuteketezwa pamoja na wavu wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, birika na tako lake; vyandarua vya ua, nguzo zake na vikalio vyake, pazia la mlango wa ua; vigingi vya hema takatifu na vya ua pamoja na kamba zake; mavazi yaliyofumwa vizuri kabisa kwa ajili ya huduma ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na ya wanawe, kwa ajili ya huduma yao ya ukuhani.” Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikaondoka mbele ya Mose. Kila mtu aliyevutwa na kusukumwa moyoni mwake alimtolea Mungu mchango wake kwa ajili ya hema la mkutano, huduma zake zote na mavazi yake matakatifu. Hivyo wote wenye moyo mkarimu, wanaume kwa wanawake, wakaleta vipini, pete za mhuri, vikuku na kila aina ya vyombo vya dhahabu; kila mtu akamtolea Mwenyezi-Mungu kitu cha dhahabu. Kila mtu alileta chochote alichokuwa nacho kama vile sufu ya rangi ya buluu zambarau na nyekundu, au kitani safi, au manyoya ya mbuzi au ngozi ya kondoo iliyotiwa rangi nyekundu. Kila mtu aliyeweza kutoa fedha au shaba aliileta kwa Mwenyezi-Mungu kama toleo lake. Tena mtu yeyote aliyekuwa na mbao za mjohoro alileta pia. Wanawake wote waliokuwa na ujuzi wa kufuma walileta vitu walivyofuma kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Na wanawake wote waliokuwa na ujuzi walisokota manyoya ya mbuzi. Viongozi walileta vito vya rangi na mawe mengine kwa ajili ya kizibao na kifuko cha kifuani; walileta pia viungo na mafuta kwa ajili ya taa, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri. Waisraeli wote, wanaume kwa wanawake, ambao walivutwa moyoni mwao kuleta chochote kwa ajili ya kazi ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwagiza Mose ifanyike, walileta vitu hivyo kwa hiari, kama mchango wa kumpa Mwenyezi-Mungu. Mose aliwaambia Waisraeli; “Tazameni! Mwenyezi-Mungu amemteua Bezaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda. Amemjaza roho yake, amempa ujuzi, akili, maarifa na ufundi, abuni michoro ya sanaa na kufanya kazi za kufua dhahabu, fedha na shaba; achonge mawe ya kupambia na mbao kwa ajili ya kazi nyingine zote za kifundi. Pia amemwongoza yeye na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani wawafundishe wengine. Amewapa ujuzi wa kufanya kila kazi ya ufundi au ifanywayo na watu wa sanaa au mafundi wa kutarizi kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kwa kutumia ufundi wowote wa msanii. “Bezaleli na Oholiabu, pamoja na kila mwanamume ambaye Mwenyezi-Mungu amemjalia uwezo na akili ya kujua namna ya kufanya kazi zote katika ujenzi wa hema takatifu, atafanya kazi kulingana na yote ambayo Mwenyezi-Mungu aliamuru.” Mose alimwita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu ambaye alikuwa amejaliwa ujuzi na Mwenyezi-Mungu, na kila mtu ambaye moyo wake ulimsukuma kufanya kazi kwa hiari. Hao wakapokea kutoka kwa Mose vitu vyote vilivyotolewa na Waisraeli kwa hiari kwa ajili ya kazi ya hema takatifu. Watu waliendelea kumletea michango yao ya hiari kila asubuhi. Watu wote wenye ujuzi waliokuwa wanafanya kazi za kila namna za kujenga hema la mkutano walitoka, kila mmoja katika kazi yake, wakamwendea Mose na kumwambia, “Watu wameleta vitu vingi zaidi ya vile vinavyohitajiwa kwa kazi aliyotuagiza Mwenyezi-Mungu tuifanye.” Basi, Mose akaagiza: “Mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, asilete mchango zaidi kwa ajili ya hema takatifu.” Watu wakazuiwa kuleta vitu, maana vile walivyokuwa wameleta vilitosha kwa kazi hiyo na kubaki. Wanaume wote wenye ujuzi walitengeneza hema takatifu kwa mapazia kumi ya kitani safi iliyosokotwa, na kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kuyatarizi viumbe wenye mabawa. Urefu wa kila pazia ulikuwa mita 12 na upana mita 2. Mapazia yote yalikuwa ya kipimo kimoja. Aliyaunga mapazia matano kufanya kipande kimoja na kufanya vivyo hivyo na yale mengine matano. Alitengeneza vitanzi vya buluu upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi vingine katika pazia la mwisho la kipande cha pili. Alitia vitanzi hamsini katika pazia la kwanza la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini kwenye utepe wa pazia la pili; vitanzi vyote vilielekeana. Kisha alitengeneza vifungo hamsini vya dhahabu ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia; hivyo, hema likawa kitu kimoja. Kisha alitengeneza pia kifuniko cha hema kwa mapazia kumi na moja ya manyoya ya mbuzi. Kila pazia lilikuwa na urefu wa mita 13, na upana wa mita 2. Mapazia yote 11 yalikuwa ya kipimo kilekile. Basi, akayaunganisha mapazia matano pamoja, na mapazia sita pamoja. Kisha alifanya vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini upindoni mwa kipande cha pili. Halafu akatengeneza vifungo hamsini vya shaba ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia, na hivyo kufanya pazia moja la hema. Kisha alitengeneza kifuniko cha ngozi laini ya kondoo dume, na juu yake kifuniko kingine cha ngozi laini ya mbuzi. Halafu akalitengenezea hema mbao za mjohoro za kusimama wima. Kila ubao ulikuwa na urefu wa mita 4 na upana wa sentimita 66. Kila ubao ulikuwa na ndimi mbili za kuunganishia. Mbao zote za hema alizifanyia ndimi. Mbao hizo za hema zilitengenezwa hivi: Mbao ishirini upande wa kusini, na vikalio arubaini vya fedha chini ya hizo mbao 20; vikalio viwili chini ya kila ubao ili kushikilia zile ndimi zake mbili. Na upande wa pili, yaani kaskazini mwa hema, alitengeneza pia mbao ishirini, na vikalio vyake arubaini vya fedha; vikalio viwili chini ya kila ubao. Upande wa nyuma, yaani magharibi mwa hema, alitengeneza mbao sita. Alitengeneza pia mbao mbili kwa ajili ya pembe za hema upande wake wa nyuma. Mbao hizo mbili za pembeni ziliachana chini lakini zilishikamanishwa kwenye pete ya kwanza. Mbao mbili kwa ajili ya hizo pembe mbili zilitengenezwa namna hiyo. Hivyo kulikuwa na mbao nane na vikalio vyake vya fedha kumi na sita, vikalio viwili chini ya kila ubao. Alitengeneza pia pau za mjohoro: Pau tano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa hema, pau tano kwa ajili ya upande wa pili wa hema, na pau tano kwa ajili ya mbao za upande wa nyuma wa hema, ulio magharibi. Alitengeneza upau wa katikati uliofika nusu ya jengo la hema ambao ulipenya katikati kutoka mwisho hadi mwisho. Mbao zote alizipaka dhahabu, akazitengeneza na pete za dhahabu za kushikilia pau hizo ambazo pia alizipaka dhahabu. Alitengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Pazia hilo lilitariziwa viumbe wenye mabawa kwa ustadi. Alitengeneza nguzo nne za mjohoro, akazipaka dhahabu na kuzitilia kulabu za dhahabu. Vilevile alizifanyia vikalio vinne vya fedha. Kadhalika, kwa ajili ya mlango wa hema, alitengeneza pazia kwa nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, nalo pazia lilitariziwa vizuri, na nguzo zake tano zikiwa na kulabu. Matumba yake na vifungo vyake alivipaka dhahabu, lakini vikalio vyake vitano vilikuwa vya shaba. Bezaleli alitengeneza sanduku kwa mbao za mjohoro; urefu wake ulikuwa sentimita 110, upana sentimita 66, na kimo chake sentimita 66. Alilipaka dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu pande zote. Kisha alitengeneza pete nne za dhahabu za kulibebea, akazitia kwenye pembe zake, kila pembe pete moja. Alitengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka dhahabu. Mipiko hiyo akaipitisha katika zile pete zilizo katika pande mbili za sanduku, kwa ajili ya kulibebea. Alitengeneza kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake sentimita 110, na upana wake sentimita 66. Alitengeneza pia viumbe wenye mabawa wawili kwa kufua dhahabu kwenye miisho ya kifuniko hicho; kiumbe kimoja mwisho huu na kingine mwisho mwingine. Alitengeneza viumbe hivyo vyenye mabawa kwenye miisho ya kifuniko hicho, vikiwa kitu kimoja na kifuniko. Viumbe hivyo vilikuwa vimeelekeana, mabawa yao yamekunjuliwa kukifunika kifuniko cha sanduku; nyuso zao zilikielekea kifuniko cha sanduku. Vilevile alitengeneza meza ya mjohoro yenye urefu wa sentimita 88, upana sentimita 44, na kimo chake sentimita 66. Aliipaka dhahabu safi na kuitengenezea ukingo wa dhahabu. Aliizungushia mviringo wa ubao wenye upana wa milimita 75, na kuifanyia ukingo wa dhahabu. Aliitengenezea pete nne za dhahabu na kuzitia katika pembe zake nne mahali miguu ilipoishia. Pete hizo za kushikilia ile mipiko ya kulibebea ziliwekwa karibu na ule mviringo wa ubao. Alitengeneza mipiko miwili ya mjohoro ya kulibebea, akaipaka dhahabu. Alitengeneza vyombo vya dhahabu safi vya kuweka juu ya meza: Sahani zake na visahani kwa ajili ya ubani, na bilauri zake na bakuli kwa ajili ya tambiko za kinywaji. Alitengeneza pia kinara cha taa kwa dhahabu safi. Tako lake, na ufito wa hicho kinara ulikuwa kitu kimoja pamoja na vikombe vyake, matumba yake na maua yake. Matawi sita yalitokeza kila upande wa ufito wake, matawi matatu upande mmoja na matawi matatu upande mwingine. Katika kila tawi kulikuwa na vikombe vitatu mfano wa maua ya mlozi, kila kimoja na tumba lake na ua lake. Na katika ufito kulikuwa na vikombe vinne mfano wa maua ya mlozi, pamoja na matumba yake na maua yake. Mahali pale palipotokezea jozi tatu za matawi chini ya kila jozi kulikuwa na tumba moja. Matumba hayo na matawi vilikuwa kitu kimoja na kinara hicho, na chote kilifuliwa kwa dhahabu safi. Alikitengenezea taa saba, koleo na visahani vyake kwa dhahabu safi. Alikitengeneza kinara hicho na vifaa vyake kwa kilo thelathini na tano za dhahabu. Alitengeneza madhabahu ya kufukizia ubani kwa mbao za mjohoro. Madhabahu hiyo ilikuwa ya mraba, sentimita 45 kwa sentimita 45, na kimo chake sentimita 90. Pembe za madhabahu hiyo zilikuwa kitu kimoja na madhabahu yenyewe. Yote aliipaka dhahabu safi: Upande wake wa juu, pande zake za ubavuni na pembe zake; pia aliitengenezea ukingo wa dhahabu. Alitengeneza pete mbili za dhahabu chini ya ukingo kwenye pande mbili zinazokabiliana. Pete hizo zilitumika kushikilia mipiko ya kuibebea. Alifanya mipiko miwili ya mjohoro na kuipaka dhahabu. Alitengeneza mafuta matakatifu ya kupaka, na ubani safi wenye harufu nzuri uliochanganywa vizuri kama manukato. Alitengeneza madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa. Madhabahu hiyo ilikuwa ya mraba, mita mbili na robo kwa mita 2.25, na kimo chake mita 1.25. Katika kila pembe ya madhabahu hiyo alitengeneza upembe uliokuwa umeundwa kutokana na madhabahu yenyewe. Madhabahu hiyo yote aliipaka shaba. Alitengeneza pia vyombo vyote kwa ajili ya madhabahu: Vyungu, sepetu, mabirika, nyuma na visahani vya kuchukulia moto. Vyombo vyake vyote alivitengeneza kwa shaba. Alitengeneza wavu wa shaba, akautia chini ya ukingo wa madhabahu hadi katikati ya madhabahu. Katika pembe nne alitengeneza pete nne za kuibebea hiyo madhabahu. Alitengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka shaba. Aliitia ile mipiko katika zile pete zilizokuwa kando ya madhabahu ili kuibebea. Madhabahu hiyo iliyotengenezwa kwa mbao ilikuwa na mvungu ndani. Kisha alitengeneza birika la shaba na tako lake la shaba; birika hilo lilitengenezwa kwa kutumia vioo vya shaba vya wanawake waliohudumu penye lango la hema la mkutano. Kisha alilitengenezea ua. Vyandarua vya upande wa kusini wa ua vilikuwa vya kitani safi iliyosokotwa na vyenye urefu wa mita 44; navyo vilishikiliwa na nguzo ishirini za shaba zenye vikalio ishirini vya shaba. Lakini kulabu za nguzo hizo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. Upande wa kaskazini urefu wa chandarua ulikuwa mita 44, na nguzo zake 20 za shaba, lakini kulabu za nguzo hizo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. Upande wa magharibi ulikuwa na chandarua chenye urefu wa mita 22, nguzo zake 10 na vikalio vyake 10. Kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. Upande wa mashariki, kulikokuwa na mlango, ulikuwa na upana wa mita 22. Chandarua cha kila upande wa mlango kilikuwa na upana wa mita 6.5, pamoja na nguzo tatu na vikalio vyake vitatu. Upande mwingine kadhalika ulikuwa na chandarua chenye upana wa mita 6.5, pamoja na nguzo tatu na vikalio vyake vitatu. Vyandarua vyote kuuzunguka ua vilikuwa vya kitani safi iliyosokotwa. Vikalio vyote vya nguzo vilikuwa vya shaba, lakini kulabu za nguzo hizo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. Matumba yake yalikuwa ya fedha; pia nguzo zake zote zilishikamanishwa kwa fito za fedha. Pazia la mlango wa ua lilitengenezwa kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri; nalo lilikuwa na urefu wa mita 9 na kimo cha mita 2, kulingana na vyandarua vya ua. Pia nguzo zake zilikuwa nne na vikalio vinne vya shaba. Kulabu zake zilikuwa za fedha, hata nguzo zake na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. Vigingi vyote vya hema na vya ua kandokando ya hema vilikuwa vya shaba. Ifuatayo ni orodha ya vifaa vilivyotumika katika kulijenga hema takatifu, yaani hema la agano. Orodha hii ilitayarishwa na Walawi kwa amri ya Mose, chini ya uongozi wa Ithamari, mwana wa kuhani Aroni. Bezaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, alifanya kila kitu ambacho Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose. Alisaidiwa na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, fundi stadi wa kutia nakshi, kusanii michoro na kutarizi kwa nyuzi za sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Dhahabu yote waliyomtolea Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya ujenzi wa hema takatifu ilikuwa na uzito wa kilo 877 na gramu 300 kulingana na vipimo vya hema takatifu. Fedha waliyochanga hao watu wa jumuiya waliohesabiwa ilikuwa ya uzito wa kilo 3,017 na gramu 750 kulingana na vipimo vya hema takatifu. Kila mtu aliyehesabiwa tangu umri wa miaka ishirini na moja na zaidi alitoa mchango wake wa fedha gramu 5; na wanaume wote waliohesabiwa walikuwa 603,550. Kilo 3,000 za fedha zilitumika kutengenezea vile vikalio 100 vya hema takatifu na lile pazia, yaani kilo 30 kwa kila kikalio. Zile kilo 17 na gramu 75 zilizosalia, zilitumika kutengenezea kulabu za nguzo na kuvipaka vichwa vya nguzo na kuitengenezea vitanzi. Jumla ya mchango wa shaba Waisraeli waliomtolea Mwenyezi-Mungu ilikuwa na uzito wa kilo 2124. Bezaleli aliitumia shaba hiyo kutengenezea vikalio vya mlango wa hema la mkutano, madhabahu ya shaba pamoja na wavu wake wa shaba, vyombo vyote vya madhabahu, vikalio vya ua uliolizunguka hema la mkutano na vya lango la ua, na vigingi vyote vya hema takatifu na vya ua. Kwa kutumia sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu walifuma sare za kuvaa wakati wa kuhudumu mahali patakatifu. Walimshonea Aroni mavazi matakatifu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Walitengeneza kizibao kwa nyuzi za dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kwa kitani safi iliyosokotwa. Waliifua dhahabu na kuikata katika nyuzi nyembamba ili kuzifuma pamoja na sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa kwa ustadi. Kizibao hicho kilivaliwa kwa kamba mbili mabegani zilizoshonewa kwenye ncha zake mbili. Mkanda uliofumwa kwa ustadi juu yake ili kuifungia ulikuwa kitu kimoja na kizibao hicho, na ulitengenezwa kwa vitu hivyohivyo: Dhahabu, sufu ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Kisha waliandaa vito vya sardoniki na kuvipanga katika vijalizo vya dhahabu; navyo vilichorwa, kama mtu achoravyo mhuri, majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. Waliviweka vito hivyo katika kanda za mabegani za kile kizibao ili kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Mafundi walitengeneza kifuko cha kifuani kama vile walivyokitengeneza kile kizibao, kwa dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, rangi zambarau na nyekundu, na kwa kitani safi iliyosokotwa. Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, sentimita 22 kwa sentimita 22 nacho kilikunjwa. Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za mawe ya thamani; safu ya kwanza ilikuwa ya akiki, topazi na almasi nyekundu; safu ya pili ilikuwa ya zumaridi, na johari ya rangi ya samawati na almasi; safu ya tatu ilikuwa ya yasintho, ya akiki nyekundu na amethisto; na safu ya nne ilikuwa ya zabarajadi, ya shohamu na yaspi; yote yalimiminiwa vijalizo vya dhahabu. Basi, palikuwa na mawe kumi na mawili yaliyochorwa majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. Yalikuwa yamechorwa kama wachoravyo mhuri, kila moja limechorwa jina kuwakilisha makabila kumi na mawili. Walikitengenezea kile kifuko cha kifuani mikufu ya dhahabu safi. Walitengeneza vijalizo viwili vya dhahabu safi na pete mbili za dhahabu, na kuzitia pete hizo kwenye ncha mbili za juu za kifuko hicho. Mikufu hiyo miwili ya dhahabu waliifunga kwenye pete hizo za kifuko cha kifuani. Zile ncha mbili za mikufu ya dhahabu walizitia kwenye vile vijalizo viwili wakazishikamanisha na vile vipande viwili vya mabegani vya kizibao, upande wa mbele. Walitengeneza pete mbili za dhahabu, wakazitia penye ncha mbili za chini upande wa ndani wa kifuko hicho cha kifuani karibu na kizibao. Walitengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzitia mbele katika ncha za chini za vipande vya kizibao, mahali kinapoungana na ule mkanda uliofumwa kwa ustadi. Walifunga kifuko cha kifuani kwenye kizibao kwa kufunganisha pete zake na kizibao kwa kamba ya rangi ya buluu, ili kifuko hicho kisilegee ila kikalie ule mkanda uliofumwa kwa ustadi, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Alitengeneza kanzu ya kuvaa ndani ya kizibao ya rangi ya buluu. Joho hilo lilikuwa na nafasi ya kupitishia kichwa katikati, nayo ilizungushiwa utepe uliofumwa ili isichanike. Kwenye upindo wa chini wa kanzu walifuma mapambo ya makomamanga ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa. Kisha walitengeneza njuga za dhahabu, na kila baada ya komamanga walitia njuga kwenye upindo wa joho. Hivyo, njuga na komamanga vilifuatana kuuzunguka upindo wa joho hilo, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Kisha wakawafumia Aroni na wanawe vizibao vya kitani safi, kilemba cha kitani safi, kofia za kitani safi, suruali za kitani safi iliyosokotwa, na mikanda ya kitani safi iliyosokotwa kwa sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu na kuitarizi vizuri, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Kisha walitengeneza pambo la dhahabu safi kwa ajili ya taji takatifu na kuchora juu yake kama wachoravyo mhuri, “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.” Kisha wakalifunga mbele ya kile kilemba kwa ukanda wa rangi ya buluu, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Basi, kazi yote ya hema la mkutano ikamalizika. Waisraeli walifanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Wakamletea Mose hema takatifu pamoja na vyombo vyake vyote, vikonyo vyake, mbao zake, pau zake, nguzo zake na vikalio vyake; kifuniko cha ngozi za kondoo dume na mbuzi kilichotiwa rangi nyekundu, pazia la mahali patakatifu, sanduku la agano, mipiko yake na kiti cha rehema; meza na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mungu; kinara cha taa cha dhahabu safi, taa zake, vyombo vyake vyote pamoja na mafuta kwa ajili ya taa hizo; madhabahu ya dhahabu; mafuta ya kupaka, ubani wenye harufu nzuri, na pazia la mlango wa hema; madhabahu ya shaba na wavu wake wa shaba, mipiko yake na vyombo vyake vyote; bakuli, birika na tako lake; vyandarua vya ua, nguzo zake na vikalio vyake; pazia la mlango wa ua, kamba zake na vigingi vyake; vyombo vyote vilivyohitajika katika huduma ya hema takatifu, yaani hema la mkutano; na mavazi yote yaliyofumwa vizuri kabisa kwa ajili ya huduma ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni, na ya wanawe kwa ajili ya huduma ya ukuhani. Waisraeli walifanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Mose alikagua kila kitu, akaridhika kwamba walikuwa wamefanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hivyo Mose akawabariki. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, utalisimika hema takatifu la mkutano. Ndani ya hema hilo utaweka lile sanduku la ushuhuda, kisha weka pazia mbele yake. Utaiingiza meza na kupanga vyombo vyake juu. Utaingiza kile kinara pia na kuziweka taa zake juu yake. Madhabahu ya dhahabu ya kufukizia ubani utaiweka mbele ya sanduku la ushuhuda, kisha utatundika pazia kwenye mlango wa hema takatifu. Ile madhabahu ya kuteketezea sadaka utaiweka mbele ya mlango wa hema takatifu la mkutano. Birika la kutawadhia utaliweka katikati ya hema la mkutano na madhabahu na kulijaza maji. Utazungushia ua na kutundika pazia penye lango lake. “Kisha, utaliweka wakfu hema takatifu pamoja na vyombo vyake vyote kwa kuvipaka yale mafuta ya kupaka, nalo litakuwa takatifu. Halafu, utaiweka wakfu madhabahu ya kuteketezea sadaka na vyombo vyake vyote kwa kuipaka mafuta, nayo itakuwa takatifu kabisa. Birika la kutawadhia na tako lake pia utaliweka wakfu kwa namna hiyohiyo. “Utamwita Aroni na wanawe waje mlangoni mwa hema la mkutano, kisha uwatawadhe. Mvike Aroni yale mavazi matakatifu; utampaka mafuta na kumweka wakfu, ili aweze kunitumikia kama kuhani. Waite wanawe na kuwavisha zile kanzu. Kisha uwapake mafuta kama ulivyompaka baba yao, ili nao pia wanitumikie kama makuhani. Kupakwa mafuta huku kutawaingiza katika ukuhani wa kudumu katika vizazi vyao vyote.” Basi, Mose alitekeleza kikamilifu kabisa maagizo yote ya Mwenyezi-Mungu. Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza mwaka wa pili baada ya kutoka Misri, hema la mkutano lilisimikwa. Mose aliweka vikalio vyake, akainua mbao zake, akashikamanisha pau zake na kusimamisha nguzo zake. Alitandaza pazia juu ya hema takatifu na kuweka kifuniko cha hema juu yake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Kisha alichukua vile vibao viwili vya mawe na kuviweka katika lile sanduku. Aliipitisha ile mipiko katika vikonyo vya sanduku na kukiweka kiti cha rehema juu yake. Kisha akaliweka lile sanduku la maamuzi ndani ya hema na kutundika pazia, na kwa namna hiyo akalisitiri sanduku la maamuzi, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Aliweka meza ndani ya hema la mkutano, upande wa kaskazini, sehemu ya nje ya pazia, na juu yake akaipanga mikate iliyotolewa kwa Mwenyezi-Mungu, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Alikiweka kinara ndani ya hema la mkutano, upande wa kusini, mkabala wa meza. Humo, mbele ya Mwenyezi-Mungu, akaziwasha taa zake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Aliiweka ile madhabahu ya dhahabu katika hema, mbele ya pazia, na kufukiza ubani wenye harufu nzuri juu yake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Alitundika pazia kwenye mlango wa hema takatifu, akaweka hapo langoni mwa hema takatifu madhabahu ya sadaka za kuteketezwa, akatolea juu yake sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Aliliweka birika la kutawadhia katikati ya hema la mkutano na madhabahu, na kutia maji ya kutawadha. Mose, Aroni na wanawe, wote walinawa mikono na miguu yao humo. Kila walipoingia ndani ya hema au walipokaribia ile madhabahu, walinawa, kama Mose alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Mwishowe Mose akatengeneza ua kulizunguka hema takatifu na madhabahu, na kuweka pazia kwenye lango la ua. Hivyo, Mose akaikamilisha kazi yote. Kisha, lile wingu likalifunika lile hema la mkutano, na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukalijaza hema. Mose alishindwa kuingia ndani ya hema la mkutano kwa sababu hilo wingu lilikaa juu yake, na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukajaa humo. Katika safari zao zote Waisraeli hawakuanza safari kamwe isipokuwa wakati wingu hilo lilipoinuliwa kutoka juu ya hema. Kama wingu hilo halikuinuliwa wao hawakuanza safari; walingoja mpaka wakati lilipoinuliwa. Katika safari zao zote, Waisraeli waliweza kuliona lile wingu la Mwenyezi-Mungu juu ya hema wakati wa mchana na ule moto ukiwaka juu yake usiku. Mwenyezi-Mungu alimwita Mose na kuongea naye katika hema la mkutano, akamwambia, “Waambie Waisraeli kwamba kama mtu anapenda kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya mnyama, mnyama huyo atamchagua kutoka kundi lake la ng'ombe, kondoo au mbuzi. “Kama sadaka anayotoa mtu ni ya kuteketezwa, atamchagua mnyama dume asiye na dosari kutoka kundi lake, atamtolea mbele ya mlango wa hema la mkutano ili apate fadhili ya Mwenyezi-Mungu; ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama wa sadaka ya kuteketezwa, ambayo itakubaliwa kwa ajili ya kumfanyia huyo mtu upatanisho. Kisha, atamchinja huyo ng'ombe mbele ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani, wazawa wa Aroni, wataichukua damu na kuinyunyizia madhabahu mlangoni mwa hema la mkutano, pande zake zote. Huyo mtu atamchuna huyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa na kumkata vipandevipande. Hao makuhani wazawa wa Aroni watazipanga kuni juu ya madhabahu na kuwasha moto. Kisha makuhani hao watachukua vile vipande vya nyama, kichwa na mafuta, na kuviweka juu ya kuni juu ya madhabahu. Lakini matumbo na miguu ya mnyama huyo mtu ataviosha kwa maji. Kuhani ataiteketeza sadaka yote juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. “Kama sadaka yake ya kuteketezwa ataitoa katika kundi la kondoo au mbuzi, basi, atachagua dume asiye na dosari. Atamchinjia upande wa kaskazini wa madhabahu, mbele ya Mwenyezi-Mungu, hao makuhani, wazawa wa Aroni watainyunyizia madhabahu damu pande zake zote. Kisha huyo mtu atamkata vipandevipande, akivitenga kichwa pamoja na mafuta yake, na kuhani ataviweka kwenye moto juu ya madhabahu. Lakini matumbo na miguu yake ataviosha kwa maji. Kuhani ataiteketeza yote juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. “Ikiwa anamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa ya ndege, basi, ataleta sadaka yake ya hua au kinda la njiwa. Kuhani atamleta ndege huyo kwenye madhabahu, atamkongonyoa kichwa chake na kukiteketeza juu ya madhabahu. Damu yake itanyunyiziwa ubavuni mwa madhabahu. Kibofu chake pamoja na uchafu wake ataviondoa na kutupa upande wa mashariki wa madhabahu ambako majivu huwekwa. Atamshika mabawa na kumpasua, lakini asimkate vipande viwili. Kisha, kuhani atamteketeza kwenye madhabahu, juu ya kuni. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.” “Mtu yeyote akileta sadaka ya nafaka kwa Mwenyezi-Mungu, sadaka hiyo iwe ya unga laini. Atautia mafuta na ubani. Kisha, atawaletea hao makuhani wa ukoo wa Aroni. Atachukua konzi moja ya unga huo laini wenye mafuta na ubani na kumpelekea kuhani mmojawapo ambaye atauteketeza juu ya madhabahu uwe sadaka ya ukumbusho kwa Mwenyezi-Mungu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Sehemu inayobaki ya sadaka hiyo ni ya makuhani. Hiyo ni sehemu takatifu kabisa ya sadaka anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. “Kama mtu anamtolea Mungu sadaka ya nafaka iliyookwa jikoni, hiyo itakuwa ya mikate isiyotiwa chachu ya unga laini uliochanganywa na mafuta ya zeituni, au ya mikate myembamba isiyo na chachu na isiyopakwa mafuta. Iwapo sadaka unayotoa ni ya mkate uliookwa kwenye kikaango, hiyo itakuwa ya unga laini uliochanganywa na mafuta ya zeituni lakini bila chachu. Mikate hiyo itakatwakatwa na kumiminiwa mafuta; hiyo ni sadaka ya nafaka. Kama sadaka unayotoa ni ya mikate iliyopikwa katika sufuria, hiyo itakuwa ya unga laini na imetiwa mafuta. Utaleta sadaka ya nafaka iliyotengenezwa kwa vitu hivyo mbele ya Mwenyezi-Mungu; na kuhani ataipeleka kwenye madhabahu. Kuhani atachukua sehemu ya sadaka hiyo ikiwa ni sadaka ya ukumbusho na kuiteketeza juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Sehemu inayobaki ya sadaka ya nafaka, ni ya makuhani. Hiyo ni sehemu takatifu kabisa ya sadaka inayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. “Sadaka yoyote ya nafaka utakayomletea Mwenyezi-Mungu ni lazima iwe imetengenezwa bila chachu; kwani hakuna ruhusa kamwe kutumia chachu wala asali katika sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Unaweza kumletea Mwenyezi-Mungu mazao yako ya kwanza kama sadaka. Lakini hayo hayatatolewa madhabahuni kama harufu ya kumpendeza. Utakoleza sadaka zako zote za nafaka kwa chumvi. Kamwe usiache kuweka chumvi katika sadaka yako ya nafaka, kwani chumvi ni ishara ya agano alilofanya Mungu pamoja nanyi. “Ukimtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya mazao yako ya kwanza utaitoa hiyo ikiwa imechomwa katika masuke yake, au utaitoa katika mikate ya kuokwa iliyotengenezwa kwa ngano iliyosagwa. Utaitia mafuta na kuweka ubani; hiyo ni sadaka ya nafaka. Kuhani ataiteketeza sehemu ya sadaka hiyo ya nafaka iliyopondwa na mafuta pamoja na ubani wake wote, iwe sadaka ya ukumbusho; hiyo ni sadaka anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. “Kama mtu anatoa sadaka ya amani, na sadaka yake ni ng'ombe dume au jike basi, mnyama huyo asiwe na dosari mbele yangu. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama huyo na kumchinja mlangoni mwa hema la mkutano. Hao makuhani wazawa wa Aroni watainyunyizia madhabahu damu yake pande zake zote. Mafuta yote yanayofunika na yaliyo juu ya matumbo ya mnyama wa sadaka hiyo ya amani atayateketeza kama sadaka anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Atatoa pia zile figo mbili na mafuta yake pamoja na ile sehemu bora ya ini. Wazawa wa Aroni wataiteketeza madhabahuni pamoja na sadaka ya kuteketezwa iliyoko juu ya kuni; hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. “Kama sadaka hiyo ya kufanya amani unayomtolea Mwenyezi-Mungu ni kutoka kundi la kondoo au mbuzi, basi achaguliwe dume au jike asiye na dosari. Kama mtu atatoa mwanakondoo kuwa sadaka yake, basi, atamtolea mbele ya Mwenyezi-Mungu, akiweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama huyo na kumchinja mbele ya hema la mkutano. Makuhani wazawa wa Aroni watainyunyizia madhabahu damu yake pande zake zote. Kisha, kutoka katika sadaka hiyo ya amani anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto, atamtolea sehemu zifuatazo: Mafuta yake, mkia wenye mafuta mzima uliokatwa karibu kabisa na uti wa mgongo pamoja na mafuta yote yanayofunika matumbo na mafuta yote yaliyo kwenye matumbo, zile figo mbili na mafuta yake pamoja na sehemu bora ya ini. Kuhani ataviteketeza hivyo vyote juu ya madhabahu kama chakula anachotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. “Kama sadaka yake ni mbuzi, basi, atamtolea mbele ya Mwenyezi-Mungu akiweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama huyo na kumchinja mbele ya hema la mkutano. Wazawa wa Aroni watainyunyizia madhabahu damu yake pande zake zote. Kisha, mafuta yote yanayofunika matumbo na zile figo mbili na mafuta yake pamoja na sehemu bora ya ini, atamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu kama chakula kinachotolewa kwa Mwenyezi-Mungu kwa moto kutoa harufu ya kumpendeza Mungu. Mafuta yote ni ya Mwenyezi-Mungu. Ndiyo maana siku zote na mahali popote mtakapokaa ni lazima kushika kanuni hii. Kamwe msile mafuta wala damu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie watu wa Israeli hivi: Kama mtu ametenda dhambi bila kukusudia, akafanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu, atafanya kama ifuatavyo: Ikiwa kuhani ambaye amepakwa mafuta ndiye aliyetenda dhambi hata akawatia watu hatiani, basi huyo atamtolea Mwenyezi-Mungu fahali mchanga asiye na dosari awe sadaka ya kuondoa dhambi. Atamleta huyo fahali mchanga kwenye mlango wa hema la mkutano, mbele ya Mwenyezi-Mungu; naye ataweka mkono wake juu ya kichwa cha fahali huyo na kumchinja mbele ya Mwenyezi-Mungu. Huyo kuhani, aliyepakwa mafuta atachukua kiasi cha damu na kuingia nayo ndani ya hema la mkutano. Atachovya kidole chake katika damu hiyo na kuirashia mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu upande wa mbele wa pazia la mahali patakatifu. Kuhani atachukua sehemu ya damu na kuzipaka pembe za madhabahu ya kufukizia ubani wa harufu nzuri, mbele ya Mwenyezi-Mungu katika hema la mkutano. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka iliyoko karibu na mlango wa hema la mkutano. Kisha atayaondoa mafuta yote ya ng'ombe huyo: Mafuta yanayofunika matumbo, figo mbili na mafuta yaliyo juu yake na yale yaliyo kiunoni, na yale yaliyoshikamana na figo na ini; hizi ni sehemu zilezile zinazoondolewa kwa mnyama wa sadaka ya amani. Kuhani atazichukua na kuziteketeza juu ya madhabahu ya kuteketezea sadaka. Lakini ngozi ya huyo ng'ombe, nyama, kichwa, miguu, matumbo na mavi yake, yaani ng'ombe mzima aliyesalia atampeleka na kumteketeza nje ya kambi mahali safi ambapo majivu hutupwa, naye atamchoma kwa moto juu ya kuni; atachomwa moto hapo mahali pa kumwagia majivu. “Iwapo jumuiya yote nzima ya Israeli imetenda dhambi bila ya kukusudia kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu mara dhambi hiyo itakapojulikana, jumuiya yote itatoa fahali mchanga awe sadaka ya kuondoa dhambi. Watamleta kwenye hema la mkutano. Wazee wa jumuiya ya watu wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo fahali, kisha atachinjwa mbele ya Mwenyezi-Mungu. Yule kuhani aliyeteuliwa rasmi kwa kupakwa mafuta ataleta sehemu ya damu ya huyo fahali ndani ya hema la mkutano. Atachovya kidole chake katika hiyo damu na kuinyunyiza mbele ya pazia mara saba, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kisha, sehemu ya damu atazipaka pembe za madhabahu iliyoko katika hema la mkutano mbele ya Mwenyezi-Mungu. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka iliyo karibu na mlango wa hema la mkutano. Mafuta yote ya mnyama huyo atayachukua na kuyateketeza kwenye madhabahu. Kwa hiyo atamfanya fahali huyu kama alivyomfanya yule mwingine wa sadaka ya kuondoa dhambi. Basi, huyo kuhani atawafanyia watu ibada hiyo ya upatanisho kwa ajili ya dhambi, nao watasamehewa. Kisha atamchukua fahali huyu na kumpeleka nje ya kambi na kumteketeza kwa moto kama alivyomfanya yule mwingine. Hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi ya jumuiya. “Ikiwa mtawala ametenda dhambi bila kukusudia kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, na hivyo akawa na hatia, mara akijulishwa dhambi hiyo aliyotenda, ataleta sadaka yake ya beberu asiye na dosari. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha beberu na kumchinjia mahali wanapochinjia sadaka za kuteketezwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi. Kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka. Mafuta yote ya beberu huyo atayateketeza madhabahuni, kama afanyavyo na mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa hiyo kuhani atamfanyia mtawala ibada hiyo ya upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa. “Kama mtu wa kawaida ametenda dhambi bila kukusudia, kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu na hivyo akawa na hatia, mara atakapojulishwa kuwa ametenda dhambi, ataleta sadaka ya mbuzi jike asiye na dosari kwa ajili ya kuondoa dhambi aliyotenda. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mbuzi huyo wa sadaka ya kuondoa dhambi, na kumchinjia mahali wanapochinjia wanyama wa sadaka za kuteketezwa. Kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu iliyobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu. Mafuta yote ya mbuzi huyo atayaondoa kama aondoavyo mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, naye kuhani atayateketeza madhabahuni, na harufu yake nzuri itampendeza Mwenyezi-Mungu. Basi, kuhani atamfanyia huyo mtu hiyo ibada ya upatanisho, naye atasamehewa. “Ikiwa mtu huyo ataleta mwanakondoo kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, basi, ataleta mwanakondoo jike asiye na dosari. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mwanakondoo huyo wa sadaka ya kuondoa dhambi, na kumchinjia mahali pale wanapochinjia wanyama wa sadaka za kuteketezwa. Kisha kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu. Kisha atayaondoa mafuta yote kama aondoavyo mafuta ya mwanakondoo wa sadaka ya amani, na kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka zitolewazo kwa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Naye kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa.” “Kama mtu yeyote akitakiwa kutoa ushahidi kwenye baraza juu ya jambo aliloona au kulisikia naye akakataa kusema kitu, basi, huo ni uovu na atauwajibikia. Au kama mtu yeyote miongoni mwenu amekuwa najisi bila kukusudia kwa kugusa kitu chochote najisi, iwe ni mzoga wa mnyama wa porini au wa kufugwa au wadudu, atakuwa na hatia. Au mtu akigusa chochote kilicho najisi cha binadamu, kiwe kiwacho, ambacho humfanya mtu kuwa najisi, naye hana habari, basi, atakapojua atakuwa na hatia. Au, kama mtu akiapa kufanya chochote kile, chema au kibaya, kama wafanyavyo watu bila kufikiri, atakapojua atakuwa na hatia. Basi, mtu akiwa na hatia kuhusu mambo hayo lazima akiri dhambi yake aliyotenda na kumletea Mwenyezi-Mungu sadaka yake ya kuondoa hatia. Kwa ajili ya dhambi aliyotenda ataleta kondoo jike au mbuzi jike kutoka kundi lake amtoe sadaka kwa ajili ya kuondoa dhambi. Naye kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake. “Lakini kama hawezi kutoa mwanakondoo wa sadaka ya kuondoa hatia kwa ajili ya dhambi aliyotenda, basi atamletea Mwenyezi-Mungu hua wawili au makinda mawili ya njiwa: Mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Atawaleta kwa kuhani, naye kuhani atamtoa mmoja awe sadaka ya kuondoa dhambi kwa kumkongonyoa shingo yake bila kukichopoa kichwa chake. Sehemu ya damu yake ataipaka pembeni mwa madhabahu na ile nyingine ataimimina chini kwenye tako la madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi. Kisha atamtoa yule wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa kulingana na maagizo. Kuhani atamfanyia huyo mtu upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa. “Ikiwa hawezi kutoa hua wawili au makinda mawili ya njiwa kama sadaka yake ya kuondoa dhambi aliyotenda, basi, ataleta unga kilo moja. Lakini hatautia mafuta wala ubani kwani ni sadaka ya kuondoa dhambi. Atamletea kuhani, naye atachukua unga huo konzi moja na kuuteketeza juu ya madhabahu kama sehemu ya ukumbusho, pamoja na sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi. Basi, kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho kwa ajili ya dhambi, naye atasamehewa. Unga unaobaki utakuwa wake kuhani kama ifanyikavyo kuhusu sadaka ya nafaka.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Kama mtu yeyote akikosa kwa kutenda dhambi bila kujua kuhusu kutotoa vitu vitakatifu anavyotolewa Mwenyezi-Mungu, atamletea kondoo dume asiye na dosari kutoka kundi lake. Wewe utapima thamani yake kulingana na kipimo rasmi cha mahali patakatifu. Hiyo ni sadaka ya kuondoa hatia. Zaidi ya hayo, huyo mtu atalipa madhara yote aliyosababisha kuhusu vitu vitakatifu kwa kuongeza sehemu ya tano ya thamani yake na kumpatia kuhani yote. Basi, kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa huyo kondoo dume aliye sadaka ya kuondoa hatia, naye atasamehewa. “Mtu yeyote akitenda dhambi bila kujua, kwa kuvunja amri yoyote ya Mwenyezi-Mungu, yeye ana hatia, na atalipa adhabu ya hatia yake. Atamletea kuhani kondoo dume asiye na dosari kutoka kundi lake akiwa na thamani sawa na ile ya sadaka ya hatia. Na kuhani atamfanyia upatanisho kwa kosa alilofanya, naye atasamehewa. Hiyo ni sadaka ya hatia; yeye ana hatia mbele ya Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Ikiwa mtu yeyote ametenda dhambi na kumwasi Mwenyezi-Mungu kwa kumdanganya jirani yake juu ya amana au dhamana aliyowekewa, au kumnyanganya au amemdhulumu mwenzake, au amepata kitu cha jirani yake kilichopotea, akasema kwamba hakukiona, au ameapa uongo juu ya chochote ambacho watu hufanya wakawa na hatia, mtu huyo anapokuwa ametenda dhambi na amekuwa na hatia, ni lazima arudishe alichoiba au alichopata kwa dhuluma, au amana aliyopewa, au kitu cha jirani yake kilichopotea akakipata, au chochote alichoapa kwa uongo. Atalipa kila kitu kikamilifu na kuongeza sehemu ya tano ya thamani yake. Mara atakapojua kosa lake atamrudishia mwenyewe. Kisha atamletea kuhani kondoo dume au mbuzi dume asiye na dosari amtolee Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuondoa hatia; thamani ya mnyama huyo itakuwa ile ya kawaida ya kuondoa hatia. Kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye atasamehewa kosa ambalo alikuwa amelifanya.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mpe Aroni na wanawe maagizo haya: Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka ya kuteketezwa. Sadaka ya kuteketezwa itakuwa motoni juu ya madhabahu usiku kucha hadi asubuhi na moto wake uchochewe, usizimike. Kisha kuhani akiwa amevaa vazi lake rasmi la kitani na kaptura yake ya kitani, atachukua majivu ya ile sadaka kutoka madhabahuni na kuyaweka kando ya madhabahu. Halafu baada ya kubadilisha mavazi yake atayapeleka yale majivu nje ya kambi mahali palipo safi. Moto wa madhabahu lazima uendelee kuwaka, na wala usizimwe. Kila siku asubuhi kuhani ataweka kuni kwenye moto huo na juu yake atapanga sadaka ya kuteketezwa, kabla ya kuteketeza mafuta ya sadaka ya amani. Moto utaendelea kuwaka daima juu ya madhabahu bila kuzimishwa kamwe. “Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka ya nafaka. Wazawa wa Aroni ndio walio na uwezo wa kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka hiyo juu ya madhabahu. Mmoja wa makuhani atachukua konzi moja ya unga wa sadaka ya nafaka pamoja na mafuta na ubani wote na kuviteketeza juu ya madhabahu kama sehemu ya ukumbusho; harufu yake itampendeza Mwenyezi-Mungu. Unga uliosalia atakula Aroni na wazawa wake makuhani bila kutiwa chachu. Wataula kwenye mahali patakatifu uani mwa hema la mkutano. Kamwe usiokwe pamoja na chachu. Nimewapa wao sehemu hiyo kutoka sadaka wanazonitolea kwa moto. Ni sadaka takatifu kabisa kama zilivyo sadaka za kuondoa dhambi na za kuondoa hatia. Wazawa wa kiume wa Aroni ndio peke yao wanaoruhusiwa kula sehemu hiyo maana hiyo imetengwa daima kwa ajili yao kutoka sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Yeyote atakayezigusa atakuwa mtakatifu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Tangu wakati wa kuwekwa wakfu kwa Aroni na wazawa wake wanapaswa kumtolea Mwenyezi-Mungu kilo moja ya unga laini kwa siku, nusu moja ya unga huo ataitoa asubuhi na nusu nyingine jioni. Unga huo utachanganywa na mafuta na kuokwa; kisha utauleta ukiwa vipandevipande na kumtolea Mwenyezi-Mungu; na harufu ya sadaka yake itampendeza Mungu. Kuhani aliye mzawa wa Aroni ambaye amepakwa mafuta kushika nafasi yake atamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka hiyo; hilo ni agizo la milele. Sadaka yote itateketezwa. Sadaka yoyote ya nafaka iliyotolewa na kuhani itateketezwa yote; haitaliwa kamwe.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mwambie Aroni na wanawe kuwa ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka ya kuondoa dhambi, mahali pale ambapo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa ndipo atakapochinjiwa mnyama wa sadaka ya kuondoa dhambi, mbele ya Mwenyezi-Mungu; hiyo ni sadaka takatifu kabisa. Kuhani anayetolea sadaka hiyo ndiye atakayeila. Italiwa mahali patakatifu, uani mwa hema la mkutano. Chochote kitakachogusa nyama hiyo kitakuwa kitakatifu; vazi lolote likidondokewa na damu ya sadaka hiyo, basi, vazi hilo litaoshewa mahali patakatifu. Sadaka hiyo ikichemshiwa katika vyombo vya udongo, vyombo hivyo vitavunjwa. Lakini ikiwa vyombo hivyo ni vya shaba, basi, vitasafishwa na kusuzwa kwa maji. Wanaoruhusiwa kuila ni wanaume wa ukoo wa makuhani peke yao kwa vile hiyo ni sadaka takatifu kabisa. Lakini kama damu ya sadaka yoyote ya kuondoa dhambi imeletwa ndani ya hema la mkutano ili kufanyia ibada ya upatanisho katika mahali patakatifu, sadaka hiyo itateketezwa kwa moto.” “Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka ya kuondoa hatia. Sadaka hiyo ni takatifu kabisa. Mnyama wa sadaka ya kuondoa hatia atachinjiwa mahali wanapochinjiwa wanyama wa sadaka za kuteketezwa, na damu yake itarashiwa madhabahu pande zake zote. Mafuta yake yote: Mafuta ya mkia na yale yanayofunika matumbo yatatolewa na kuteketezwa pamoja na zile figo mbili pamoja na mafuta yake na ile sehemu bora ya ini. Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu kama sadaka anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hiyo ni sadaka ya kuondoa hatia. Wanaoruhusiwa kula sadaka hiyo ni wanaume wa ukoo wa makuhani peke yao; ni sadaka takatifu kabisa. Italiwa katika mahali patakatifu. Sheria ni moja kuhusu sadaka ya kuondoa hatia na sadaka ya kuondoa dhambi: Kuhani anayefanya ibada ya upatanisho ndiye atakayeichukua. Kuhani anayetoa sadaka ya kuteketezwa ya mtu yeyote, atachukua ngozi ya mnyama aliyetolewa. Sadaka yoyote ya nafaka iliyookwa jikoni au katika sufuria au katika kikaango itakuwa mali ya kuhani anayeitoa. Kila sadaka ya nafaka, iwe imechanganywa na mafuta au kavu, itakuwa ya wazawa wa Aroni, na wote wagawiwe kwa sawa. “Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka za amani ambazo mtu aweza kumtolea Mwenyezi-Mungu. Ikiwa mtu anatoa sadaka hiyo ya kumshukuru Mungu, basi, ataitoa pamoja na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyopakwa mafuta, mikate myembamba iliyopakwa mafuta na maandazi ya unga laini uliochanganywa na mafuta. Pamoja na sadaka hiyo yake ya amani ya kumshukuru Mungu, ataleta maandazi yaliyotiwa chachu. Kutokana na maandazi hayo, atamtolea Mwenyezi-Mungu andazi moja kutoka kila sadaka; maandazi hayo yatakuwa yake kuhani anayeirashia madhabahu damu ya sadaka za amani. Nyama ya sadaka hiyo ya amani ya kumshukuru Mungu italiwa siku hiyohiyo inapotolewa; hataacha hata sehemu yake hadi asubuhi. Lakini kama sadaka hiyo ya amani ni ya nadhiri au ya hiari, italiwa siku hiyohiyo inapotolewa na sehemu nyingine yaweza kuliwa kesho yake. Lakini nyama yoyote ya sadaka hiyo inayobaki hadi siku ya tatu itateketezwa. Tena nyama yoyote ya sadaka ya amani ikiliwa siku ya tatu, haitakubaliwa, wala haitapokelewa kwa faida yake mtu aliyeitoa. Nyama hiyo ni chukizo na mtu atakayeila atawajibika kwa uovu wake. “Nyama yoyote inayogusa kitu najisi isiliwe. Nyama hiyo itateketezwa kwa moto. Wote walio safi wanaweza kula nyama iliyotolewa sadaka ya amani kwa Mwenyezi-Mungu. Lakini mtu yeyote aliye najisi, akila nyama hiyo, atatengwa na watu wake. Mtu yeyote anayegusa kitu chochote kilicho najisi, au kitu najisi cha mtu, au mnyama aliye najisi, au kitu chochote najisi ambacho ni chukizo, akila nyama ya sadaka ya amani aliyotolewa Mwenyezi-Mungu, mtu huyo atatengwa na watu wake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Msile mafuta ya ng'ombe au ya kondoo au ya mbuzi. Mafuta ya mnyama yoyote aliyekufa mwenyewe au ya mnyama aliyeuawa na mnyama wa porini yaweza kuwekwa kwa matumizi mengine, lakini kamwe msiyale. Mtu yeyote akila mafuta ya mnyama aliyetolewa kwa Mwenyezi-Mungu kwa moto, atatengwa na watu wake. Tena, kamwe msile damu yoyote ile, iwe ya ndege au ya mnyama mahali popote mnapoishi. Mtu yeyote akila damu yoyote, atatengwa na watu wake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie watu wa Israeli hivi: Mtu yeyote akitoa sadaka ya amani, atampa Mwenyezi-Mungu sehemu ya sadaka hiyo. Atamletea kwa mikono yake mwenyewe kama sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Ataleta mafuta yake pamoja na kidari ambacho atafanya nacho ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu. Kuhani atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, lakini kidari kitakuwa cha Aroni na wanawe makuhani. Mguu wa kulia wa nyuma wa mnyama wa sadaka zenu za amani mtampa kuhani. Mguu huo utakuwa mali ya kuhani aliye mzawa wa Aroni anayetoa damu ya sadaka za amani na mafuta yake. Mwenyezi-Mungu amewaagiza watu wa Israeli watenge kidari hicho na mguu huo wa mnyama wa sadaka zao za amani, wampe kuhani Aroni na wazawa wake, maana sehemu hiyo wamewekewa hao makuhani milele. Hiyo ndiyo sehemu iliyotengwa kwa ajili ya Aroni na wanawe kutoka katika sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto, tangu siku walipotawazwa kuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu. Walipowekwa wakfu kwa kupakwa mafuta, Mwenyezi-Mungu aliamuru Waisraeli wawape sehemu hiyo ya sadaka; hiyo itakuwa daima haki yao.” Basi, hayo ndiyo maagizo kuhusu sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka, sadaka ya kuondoa dhambi, sadaka ya kuondoa hatia, kuhusu kuwekwa wakfu na kuhusu sadaka ya amani. Mwenyezi-Mungu alimpa Mose amri hizi mlimani Sinai siku ile alipowaamuru Waisraeli wamletee sadaka zao, kule jangwani Sinai. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mwite Aroni na wanawe wakutane mbele ya mlango wa hema la mkutano; chukua mavazi matakatifu, mafuta ya kupaka, ng'ombe wa sadaka ya kuondolea dhambi, kondoo madume wawili, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu. Kisha, ikusanye jumuiya yote ya Waisraeli mbele ya mlango wa hema la mkutano.” Mose akafanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, akaikusanya jumuiya yote mbele ya mlango wa hema la mkutano. Mose akaiambia jumuiya yote hivi: “Lifuatalo ni jambo ambalo Mwenyezi-Mungu ameamuru lifanywe.” Hapo Mose akawaleta Aroni na wanawe na kuwatawadha. Kisha akamvika Aroni joho na kuifunga kwa mkanda, akamvika kanzu, akamvalisha kizibao na kukifunga kiunoni mwake kwa mkanda uliofumwa kwa ustadi. Kisha akaweka kifuko kifuani pa Aroni na ndani ya kifuko hicho akatia mawe ya kauli. Halafu akamvika Aroni kilemba na upande wa mbele wa kilemba hicho akaweka pambo la dhahabu, taji takatifu, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru. Kisha Mose akachukua mafuta ya kupaka, akaipaka ile maskani na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake akaviweka wakfu. Alinyunyiza sehemu ya mafuta hayo juu ya madhabahu mara saba, akaipaka mafuta na vyombo vyake vyote, birika na tako lake, kuviweka wakfu. Vilevile Mose akampaka Aroni mafuta kichwani ili kumweka wakfu. Kisha Mose akawaleta wana wa Aroni akawavika joho na kuwafunga mikanda viunoni, na kuwavisha kofia kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Kisha Mose akamleta ng'ombe wa sadaka ya kuondoa dhambi, naye Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha ng'ombe huyo. Mose akamchinja huyo ng'ombe, akachukua damu akazipaka pembe za madhabahu pande zote kwa kidole chake kuitakasa. Kisha akachukua damu iliyobaki akaimwaga chini kwenye tako la madhabahu ambayo aliweka wakfu kwa kuifanyia ibada ya upatanisho. Kisha, akachukua mafuta yote yaliyokuwa kwenye matumbo yake, sehemu bora ya ini pamoja na figo zote mbili na mafuta yake na kuviteketeza juu ya madhabahu. Lakini nyama ya ng'ombe huyo, ngozi yake na mavi yake, akaviteketeza kwa moto nje ya kambi kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Kisha, Mose akamleta kondoo dume wa sadaka ya kuteketezwa. Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha kondoo huyo. Mose akamchinja na damu ya kondoo huyo akairashia madhabahu pande zake zote. Alimkata huyo kondoo vipandevipande, akaviteketeza pamoja na kichwa chake na mafuta yake. Baada ya matumbo na miguu kuoshwa kwa maji, Mose aliviteketeza vyote juu ya madhabahu pamoja na sehemu nyingine za huyo kondoo kama sadaka ya kuteketezwa. Hiyo ni sadaka itolewayo kwa moto, yenye harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Mose alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Kisha akamleta kondoo dume mwingine, kwa ajili ya kuweka wakfu. Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha kondoo huyo. Mose akamchinja. Akachukua damu ya kondoo huyo na kumpaka Aroni kwenye ncha ya sikio lake la kulia, kidole gumba cha mkono wake wa kulia na cha mguu wake wa kulia. Wanawe Aroni nao wakaja, naye Mose akawapaka kiasi cha damu kwenye ncha za masikio yao ya kulia, vidole gumba vya mikono yao ya kulia na kwenye vidole gumba vya miguu yao ya kulia. Damu nyingine akainyunyizia madhabahu pande zake zote. Kisha, akachukua mafuta yote, mkia pamoja na mafuta yake, mafuta yote yanayofunika matumbo, sehemu bora ya ini, pamoja na figo zote mbili, mafuta yake na paja la mguu wa kulia wa nyuma wa huyo kondoo dume. Kisha, kwenye kile kikapu cha mikate iliyowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu akatoa mkate mmoja usiotiwa chachu, mkate mmoja wenye mafuta na mkate mmoja mdogo, akaviweka vyote juu ya vipande vya mafuta na ule mguu. Mose akaviweka mikononi mwao Aroni na wanawe, nao wakafanya ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu. Kisha Mose akavichukua vitu hivyo vyote kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa. Hii ni sadaka ya kuwekwa wakfu, yenye harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu; ni sadaka itolewayo kwa moto. Kisha Mose akachukua kile kidari na kufanya ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu. Sehemu hiyo ya yule kondoo dume wa kuweka wakfu ni mali yake Mose kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Halafu Mose akachukua mafuta ya kupaka na damu kutoka madhabahu akamnyunyizia Aroni na wanawe hata na pia mavazi yao. Hivyo Mose akamweka wakfu Aroni na wanawe pamoja na mavazi yao. Mose akamwambia Aroni na wanawe, “Chemsheni ile nyama mbele ya mlango wa hema la mkutano, muile hapo mlangoni pamoja na mkate kutoka katika kikapu chenye sadaka za kuwekea wakfu. Fanyeni kama nilivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, kwamba sehemu hiyo italiwa na Aroni na wanawe. Nyama yoyote au mkate wowote utakaosalia ni lazima kuteketezwa. Hamtatoka nje ya mlango wa hema la mkutano kwa muda wote wa siku saba, yaani mpaka muda wenu wa kuwekwa wakfu umekwisha, muda ambao utachukua siku saba. Mwenyezi-Mungu ameamuru tufanye kama tulivyofanya leo ili tuwafanyieni ibada ya upatanisho. Mtabaki mlangoni mwa hema la mkutano usiku na mchana kwa muda wa siku saba, mkifanya mambo aliyoamuru Mwenyezi-Mungu, la sivyo mtakufa. Ndivyo nilivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.” Basi, Aroni na wanawe wakafanya mambo yote aliyoamuru Mwenyezi-Mungu kwa njia ya Mose. Siku ya nane baada ya siku saba za kuwekwa wakfu, Mose akamwita Aroni na wanawe pamoja na wazee wa Israeli. Mose akamwambia Aroni, “Chukua ndama dume kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; wanyama wote wasiwe na dosari. Kisha watoe sadaka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Waambie Waisraeli wachukue beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, na ndama mmoja na mwanakondoo mmoja wote wa umri wa mwaka mmoja na wasio na dosari kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, fahali mmoja na kondoo dume mmoja kwa ajili ya sadaka za amani, wakamtolee Mwenyezi-Mungu pamoja na sadaka ya nafaka iliyochanganywa na mafuta kwa maana leo Mwenyezi-Mungu atawatokea.” Waisraeli wakaleta vyote hivyo mbele ya hema la mkutano kama Mose alivyowaamuru na jumuiya yote ikaenda kusimama mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mose akawaambia, “Hili ndilo jambo ambalo Mwenyezi-Mungu aliwaamuru mlifanye ili utukufu wake uonekane kwenu.” Hapo Mose akamwambia Aroni, “Nenda kwenye madhabahu, utolee hapo sadaka yako ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuteketezwa na kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yako na kwa ajili ya watu wa Israeli. Kisha tolea hapo sadaka za watu na kuwafanyia ibada ya upatanisho kama alivyoamuru Mwenyezi-Mungu.” Basi, Aroni akaikaribia madhabahu, akamchinja yule ndama aliyemtoa awe sadaka ya kuondoa dhambi yake mwenyewe. Wanawe wakamletea damu, naye akachovya kidole chake katika damu hiyo na kuzipaka pembe za madhabahu. Damu iliyosalia akaimwaga kwenye tako la madhabahu. Lakini mafuta na figo akaviteketeza vyote juu ya madhabahu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Lakini ile ngozi akaiteketeza kwa moto nje ya kambi. Kisha Aroni akamchinja mnyama wa sadaka ya kuteketezwa. Wanawe wakamletea damu, naye akainyunyizia madhabahu pande zote. Kisha wakamletea sadaka ya kuteketezwa, kipande kimojakimoja, na kichwa; naye akaviteketeza juu ya madhabahu. Akaosha matumbo na miguu na kuiteketeza pamoja na ile sadaka ya kuteketezwa kwenye madhabahu. Kisha, Aroni akaweka mbele sadaka ya watu. Alimchukua mbuzi wa sadaka ya watu ya kuondoa dhambi, akamchinja na kumtoa sadaka ya kuondoa dhambi, kama alivyofanya kwa yule wa kwanza. Kisha akaweka mbele ile sadaka ya kuteketezwa akatolea sadaka hiyo kulingana na agizo. Kisha akaweka mbele sadaka ya nafaka akijaza konzi moja na kuiteketeza juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya kila asubuhi. Halafu Aroni akamchinja pia fahali na yule kondoo dume wa sadaka za amani kwa ajili ya watu. Wanawe wakamletea damu ambayo aliinyunyizia madhabahu pande zote. Mafuta ya fahali huyo na kondoo dume, mkia wa kondoo, mafuta yaliyofunika matumbo, figo na sehemu bora ya ini wakayaweka juu ya vidari, naye akaviteketeza kwenye madhabahu. Lakini vile vidari na ule mguu wa nyuma wa kulia, Aroni alifanya navyo ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu, kama Mose alivyoamuru. Aroni alipomaliza kutolea sadaka zote: Sadaka za kuondoa dhambi, sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, aliwainulia watu mikono, akawabariki, kisha akashuka chini. Ndipo Mose na Aroni wakaingia ndani ya hema la mkutano; walipotoka waliwabariki watu, nao utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukaonekana kwa watu wote. Mwenyezi-Mungu akawasha moto ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa na mafuta yaliyokuwa juu ya madhabahu. Watu wote walipouona huo moto walipaza sauti na kusujudu. Nao Nadabu na Abihu, wanawe Aroni, walichukua kila mmoja chetezo chake, wakaweka moto na ubani, wakamtolea Mwenyezi-Mungu moto najisi, ambao haukulingana na agizo lake Mwenyezi-Mungu. Basi, moto ukatokea mbele ya Mwenyezi-Mungu, ukawateketeza hao vijana, wakafa mbele yake. Hapo, Mose akamwambia Aroni, “Kwa tukio hili Mwenyezi-Mungu amekuonesha maana ya kile alichosema: ‘Nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwa wale walio karibu nami; nitatukuzwa mbele ya watu wote!’” Aroni akanyamaza kimya. Basi, Mose akawaita Mishaeli na Elsafani, wanawe Uzieli, baba mdogo wa Aroni, akawaambia waje kuondoa maiti za ndugu zao maskani na kuzipeleka nje ya kambi. Wakachukua maiti za ndugu zao na kuzipeleka nje ya kambi wakiwa wamevaa mavazi yao, kama Mose alivyoamuru. Kisha Mose akamwambia Aroni na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msivuruge nywele zenu na wala msirarue mavazi yenu kuomboleza, la sivyo mtakufa na kuiletea jumuiya yote ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Lakini ndugu zenu yaani jumuiya yote ya Israeli, wanaweza kuomboleza kwa sababu ya moto huo aliouleta Mwenyezi-Mungu. Msitoke nje ya mlango wa hema la mkutano, la sivyo mtakufa; kwani mafuta ya kupaka ya Mwenyezi-Mungu yangali juu yenu.” Aroni na wanawe wakafanya kama Mose alivyosema. Mwenyezi-Mungu aliongea na Aroni, akasema, “Mnapoingia ndani ya hema la mkutano, wewe na wanao msinywe divai wala kileo chochote, la sivyo mtakufa. Hii itakuwa sheria ya kudumu katika vizazi vyenu vyote. Ni lazima mtofautishe kati ya mambo matakatifu na mambo yasiyo matakatifu, kati ya mambo najisi na yasiyo najisi. Mtawafundisha Waisraeli masharti yote ambayo nimewaambia kwa njia ya Mose.” Mose akamwambia Aroni na wanawe waliosalia: Eleazari na Ithamari, “Chukueni ile sehemu ya sadaka ya nafaka iliyosalia kutoka sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto; muile karibu na madhabahu bila kutiwa chachu kwa sababu ni takatifu kabisa. Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu hiyo ni haki yako na wazawa wako kutoka katika sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hivyo ndivyo nilivyoamriwa. Lakini kidari ambacho hufanywa nacho ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu na mguu unaotolewa sadaka kama ishara, mnaweza kula mahali popote pasipo najisi. Utakula wewe, na watoto wako wa kiume na wa kike. Vitu hivyo umepewa kama haki yako na ya wazawa wako kutoka sadaka za amani za watu wa Israeli. Ule mguu uliotolewa na kidari cha sadaka ya kufanyia ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu watavileta pamoja na sadaka za mafuta zitolewazo kwa moto, ili kufanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu, viwe sadaka ya kutolewa kwa ishara. Hivyo vitakuwa vyako pamoja na wanao; ni haki yenu milele kama Mwenyezi-Mungu alivyoamuru.” Basi, Mose alichunguza kwa makini kuhusu mbuzi mmoja aliyetolewa sadaka ya kuondoa dhambi, kumbe akagundua kuwa alikwisha teketezwa. Hivyo akawakasirikia sana Eleazari na Ithamari, wana wa Aroni waliosalia, akawauliza, “Kwa nini hamkumla katika mahali patakatifu kwa vile huyo ni kitu kitakatifu kabisa na mlikuwa mmepewa huyo ili kuondoa hatia ya jumuiya na kuwafanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu? Tena, kwa vile damu yake haikuletwa ndani ya mahali patakatifu, ni dhahiri iliwapasa kumla ndani ya mahali patakatifu kama nilivyoamuru.” Aroni akamwambia Mose, “Tazama, leo wametolea sadaka yao ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuteketezwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; hata hivyo mambo haya yamenipata! Tena kama ningekula ile sadaka ya kuondoa dhambi hivi leo, je, ingekubalika mbele ya Mwenyezi-Mungu?” Mose aliposikia hayo, akaridhika. Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Wawaambie Waisraeli hivi: Kati ya wanyama wote duniani, mmeruhusiwa kula mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na ambaye hucheua. Lakini msile mnyama yeyote ambaye hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika sehemu mbili, au ambaye kwato zake zimegawanyika lakini hacheui. Msile ngamia, kwani hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika sehemu mbili. Kwenu huyo ni najisi. Pelele msimle; yeye hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika; kwenu huyo ni najisi. Sungura msimle; yeye hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika; kwenu huyo ni najisi. Nguruwe msimle; ana kwato zilizogawanyika lakini hacheui; kwenu huyo ni najisi. Kwa sababu wanyama hao ni najisi msile nyama yao wala msiguse mizoga yao. “Samaki yeyote wa baharini au mtoni mwenye mapezi na magamba, mnaweza kumla. Lakini chochote kinachoishi baharini au mitoni, ambacho hakina mapezi wala magamba, yaani viumbe vyote viendavyo majini na viumbe vingine vyote viishivyo majini ni najisi kwenu. Viumbe hivyo vitakuwa daima najisi kwenu. Msile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao kwani ni najisi. Chochote kinachoishi majini ambacho hakina mapezi na magamba ni najisi kwenu. “Ndege wote wafuatao ni najisi kwenu; hivyo msile: Tai, furukombe, kipungu, mwewe, aina zote za kozi, aina zote za kunguru, mbuni, kirukanjia, dudumizi, aina zote za kipanga, bundi, mnandi, bundi kubwa, mumbi, mwari, mderi, korongo, aina zote za koikoi, hudihudi na popo. “Wadudu wote wenye mabawa na waendao kwa miguu minne, hao ni najisi kwenu. Lakini, baadhi ya wadudu wenye mabawa na wanakwenda kwa miguu minne ya kurukia ardhini mnaweza kula. Hao ni: Kila aina ya nzige, kila aina ya senene, kila aina ya panzi na kila aina ya parare. Lakini wadudu wengine wote wenye mabawa na miguu minne ni najisi kwenu. “Kugusa wanyama fulanifulani humfanya mtu kuwa najisi; yeyote atakayegusa mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. Mtu akichukua sehemu ya mizoga yake atakuwa najisi mpaka jioni, na mavazi yake ni lazima yafuliwe. Mtu yeyote akigusa mnyama mwenye kwato zilizogawanyika lakini hacheui, mtu huyo atakuwa najisi. Wanyama wote waendao kwa vitanga vyao ingawa wana miguu minne, ni najisi kwenu; na yeyote atakayegusa mzoga wa mnyama kama huyo atakuwa najisi mpaka jioni. Mtu yeyote anayebeba mzoga atakuwa najisi, naye atasafisha mavazi yake. Hao ni najisi kwenu. “Viumbe vifuatavyo ni najisi kwenu: Kicheche, panya, kila aina ya mjombakaka, guruguru, kenge, mijusi, goromwe, na kinyonga. Hao wote ni najisi kwenu na yeyote atakayegusa mizoga yao, atakuwa najisi mpaka jioni. Ikiwa mzoga wa viumbe hao unakiangukia kitu chochote, kiwe ni kifaa cha mbao au vazi au ngozi au gunia au chombo chochote kitumiwacho kwa kusudi lolote lile, chombo hicho kitakuwa najisi mpaka jioni. Ili kukifanya kiwe safi ni lazima kukiosha kwa maji. Ikiwa mzoga wake umeangukia chombo cha udongo, basi, chochote kilicho ndani ya chombo hicho ni najisi na lazima chombo hicho kivunjwe. Chakula au kinywaji chochote kilichokuwa ndani ya chombo hicho kitakuwa najisi. Kila kitu ambacho sehemu ya mzoga imekiangukia, kitakuwa najisi. Ikiwa ni tanuri au jiko, ni lazima kivunjwe. Vitakuwa najisi navyo ni najisi kwenu. Hata hivyo, kisima au chemchemi ya maji vitakuwa safi. Lakini chochote kinachogusa mzoga kitakuwa najisi. Iwapo sehemu ya mzoga inaziangukia mbegu za kupanda, mbegu hizo hazitakuwa najisi. Lakini ikiwa mbegu zimetiwa katika maji ili kuota na sehemu yoyote ya mzoga ikaziangukia, basi, mbegu hizo ni najisi kwenu. “Iwapo mnyama yeyote mnayeruhusiwa kula, anakufa mwenyewe, yeyote atakayegusa mzoga wake, atakuwa najisi mpaka jioni. Mtu yeyote akila nyama ya mzoga huo atafua mavazi yake na atakuwa najisi mpaka jioni. Na yeyote atakayebeba mzoga huo, atafua mavazi yake, naye atakuwa najisi mpaka jioni. “Kiumbe chochote kitambaacho duniani ni najisi kwenu, kamwe msikile. Chochote kiendacho kwa tumbo lake, chochote kiendacho kwa miguu yote minne au nyayo nyingi, naam, chochote kitambaacho, kamwe msikile kwa maana ni najisi kwenu. Hivyo msije mkawa najisi kwa kula viumbe vitambaavyo na hivyo mkawa najisi. Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndimi Mungu wenu, jiwekeni wakfu na kuwa watakatifu kwa maana mimi ni mtakatifu. Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndimi niliyewatoa nchini Misri ili niwe Mungu wenu; kwa hiyo muwe watakatifu kwa maana mimi ni mtakatifu.” Hiyo basi, ndiyo sheria kuhusu wanyama, ndege na viumbe vyote hai ambavyo huishi majini na nchi kavu, ili kupambanua kati ya kisicho najisi na kilicho najisi; kinachoweza kuliwa na kisichoweza kuliwa. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie watu wa Israeli hivi: Mwanamke akipata mimba, akajifungua mtoto wa kiume, atakuwa najisi kwa muda wa siku saba kulingana na siku zake zihusikanazo na hali ya wanawake. Mtoto huyo atatahiriwa katika siku yake ya nane. Kisha mama mtoto ataendelea kuwa najisi kwa muda wa siku thelathini na tatu. Wakati huo, kamwe asiguse chochote kilichowekwa wakfu wala kuingia mahali patakatifu mpaka siku za kutakasika kwake zitakapotimia. Lakini, kama amejifungua mtoto wa kike, basi, atakuwa najisi kwa muda wa majuma mawili kama ilivyo anapokuwa katika siku zake. Ataendelea katika kutakasika kwake kwa muda wa siku sitini na sita. “Siku za kutakaswa kwake zitakapotimia, iwe amepata mtoto wa kiume au wa kike, atamletea kuhani mlangoni mwa hema la mkutano mwanakondoo wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na kinda la njiwa au hua, kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi. Kuhani atamtolea mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumfanyia huyo mama ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu. Hivyo huyo mwanamke atakuwa safi kutokana na damu yake. Huo ni mwongozo kuhusu mwanamke yeyote anayejifungua mtoto wa kiume au wa kike. “Kama hawezi kutoa mwanakondoo, basi, ataleta hua wawili au makinda mawili ya njiwa; mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuondolea dhambi. Kuhani atamfanyia mama huyo ibada ya upatanisho, naye atakuwa safi.” Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Iwapo mtu yeyote atakuwa na uvimbe au upele au kipaku mwilini mwake, ikadhihirika kwamba ni ukoma, basi, ataletwa kwa kuhani Aroni au mmoja wa wanawe aliye kuhani. Kuhani atapakagua mahali palipo na ugonjwa na ikiwa nywele za mahali hapo zimebadilika kuwa nyeupe na ugonjwa wenyewe ukionekana kuwa uko ndani zaidi ya ngozi ya mwili wake, basi, huo ni ukoma. Kuhani akimaliza kumkagua, hivyo atatangaza kuwa mtu huyo ni najisi. Lakini ikiwa kipele hicho, ingawa cheupe hakikuingia ndani sana ya ngozi na wala nywele za mahali hapo hazikubadilika kuwa nyeupe, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba. Siku ya saba, kuhani atamwangalia tena mtu huyo, na ikiwa, kulingana na uchunguzi wa kuhani, ugonjwa huo haujaenea kwenye ngozi yake, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku nyingine saba. “Kuhani atamkagua tena mtu huyo siku ya saba. Kama kulingana na uchunguzi wake, ile sehemu ya ugonjwa imefifia na ugonjwa haujaenea, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi; huo ni upele tu. Mtu huyo atafua mavazi yake, naye atakuwa safi. Lakini upele huo ukiwa umeenea kwenye ngozi, baada ya mtu huyo kujionesha kwa kuhani kwa ajili ya kutakaswa kwake, basi, atakuja tena kwa kuhani. Kuhani atamwangalia tena, na kama ule upele umeenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; huo ni ukoma. “Kama mtu ameshikwa na ukoma, ataletwa kwa kuhani. Kuhani atamwangalia na kama kuna uvimbe mweupe ambao umezifanya nywele zake ziwe nyeupe na uvimbe huo umegeuka kuwa kidonda kibichi, huo ni ukoma wa muda mrefu. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hakuna haja ya kumweka mtu huyo kwa uchunguzi kwani yu najisi tayari. Kama ukoma umemshika na umeenea mwili mzima, toka utosini hadi nyayoni kama atakavyoona kuhani, hapo kuhani atamwangalia. Kuhani akiona kuwa ukoma umemwenea mwili mzima, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi kwa sababu mwili umegeuka kuwa mweupe na hivyo mtu huyo yu safi. Lakini kukionekana mwilini mwa mtu huyo kidonda kibichi, basi, mtu huyo atakuwa najisi. Kuhani ataangalia hicho kidonda kibichi na kumtangaza kuwa ni najisi kwa sababu huo ni ukoma. Lakini hicho kidonda kikigeuka tena kuwa cheupe, mtu huyo atarudi kwa kuhani. Kuhani atamwangalia na akiona kuwa kimegeuka kuwa cheupe, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi. “Kama mtu ameshikwa na jipu, nalo limepona, lakini mahali pale lilipokuwa jipu pamegeuka kuwa uvimbe mweupe au kuwa pekundu lakini peupe kiasi, ni lazima kumwonesha kuhani. Kuhani atamwangalia huyo mtu. Kuhani akiona pamegeuka kuwa na shimo na nywele za mahali hapo zimegeuka kuwa nyeupe, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; huo ni ugonjwa wa ukoma ambao umetokana na jipu. Lakini kama kuhani atamwangalia huyo mtu na kuona kuwa nywele za mahali hapo si nyeupe na wala hakuna shimo, ila pamefifia, basi, atamtenga huyo mtu kwa muda wa siku saba. Kama ugonjwa huo utaenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; sehemu hiyo ina ugonjwa. Lakini, kama ile sehemu haijaenea, basi, lile ni kovu la jipu tu. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi. “Au, Iwapo kuna mahali palipoungua na ile nyama mbichi imegeuka kuwa nyekundu-nyeupe au ni nyeupe, kuhani atapaangalia. Kama akiona kuwa nywele zimegeuka kuwa nyeupe na pana shimo, basi, huo ni ukoma. Ukoma huo umejitokeza kwa njia ya mahali hapo palipoungua. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani anao ugonjwa wa ukoma. Lakini kama kuhani akiona kuwa nywele za mahali hapo si nyeupe na hakuna shimo ila pamefifia, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba. Siku ya saba kuhani atamwangalia. Kama umeenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani anao ugonjwa wa ukoma. Lakini, kama ile alama haijaenea, ila imefifia, huo ni uvimbe uliotokana na kuungua; basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi; kwani hilo ni kovu la kuungua. “Kama mtu yeyote mwanamume au mwanamke, ana kidonda kichwani au kidevuni, kuhani atauangalia ugonjwa huo. Iwapo kuhani ataona kuwa kuna shimo na nywele ni manjano na nyembamba, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani huo ni upele na ni ukoma wa kichwa au wa kidevu. Kama kuhani ataona kuwa hakuna shimo na nywele si nyeusi, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba. Siku ya saba kuhani atakiangalia kile kidonda. Kama kidonda hicho hakijaenea na hakuna nywele zenye rangi ya manjano wala hakuna vipele vyovyote mahali hapo, basi, mtu huyo atanyoa nywele au ndevu zake. Lakini mahali pale penye vipele hatapanyoa. Kisha kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda mwingine wa siku saba. Siku ya saba, kuhani ataviangalia vile vipele. Iwapo kuhani ataona kuwa vipele hivyo havikuenea kwenye ngozi na wala havikwenda ndani ya ngozi, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi. Mtu huyo atafua mavazi yake, naye atakuwa safi. Lakini iwapo vipele hivyo vimeenea baada ya kutakaswa, mtu huyo ataangaliwa na kuhani na ikiwa vimeenea kwenye ngozi, kuhani hatahitaji kutafuta nywele zenye rangi manjano; mtu huyo atakuwa najisi. Lakini iwapo kuhani ataona kuwa vile vipele vimepona na nywele nyeusi zimeota mahali hapo, basi, vidonda hivyo vimepona, basi, mtu huyo ni safi. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi. “Kama mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, ana alama nyeupe mwilini mwake, kuhani atamwangalia mtu huyo. Iwapo kuhani ataona kuwa alama hizo ni nyeupe kiasi, huo ni upele wa kawaida; mtu huyo ni safi. “Kama mwanamume amepata upara, yeye ni safi kwani ana upara tu. Iwapo upara huo umetanda tangu nyuma mpaka mbele mtu huyo ana upara tu na yu safi. Lakini kama kwenye kichwa penye upara au kwenye paji la uso penye upara kuna alama nyekundu-nyeupe, huo ni ukoma unaotokea kwenye upara wake kichwani au kwenye paji lake. Kuhani atamwangalia. Iwapo kuhani ataona kuwa huo uvimbe ni mwekundu-mweupe kwenye upara au kwenye paji lake na unaonekana kama ukoma kwenye ngozi yake, basi, mtu huyo ana ukoma; yeye ni najisi. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Ugonjwa wake upo kwenye kichwa chake. “Mwenye ukoma yeyote atavaa nguo zilizochanika, nywele zake hatazichana, na mdomo wake wa juu ataufunika na atapaza sauti akisema, ‘Mimi ni najisi, mimi ni najisi.’ Ataendelea kuwa najisi kwa muda wote alio na ugonjwa huo. Yeye ni najisi; naye atakaa peke yake nje ya kambi.” “Kama kuna namna ya upele wa ukoma kwenye vazi, liwe la sufu au kitani, vazi hilo liwe limefumwa au limesokotwa kwa kitani au sufu au ni vazi la ngozi ya aina yoyote ile, iwapo upele huo una rangi ya kijani au nyekundu katika vazi hilo, basi, vazi hilo lina upele. Kwa hiyo ni lazima kumwonesha kuhani. Kuhani atauangalia upele huo na kuliweka vazi hilo kando kwa muda wa siku saba. Siku ya saba atauangalia upele huo. Ikiwa upele huo umeenea katika vazi hilo, liwe ni la kufuma au kusokotwa au la ngozi au la ngozi ya aina yoyote ile, vazi hilo lina upele. Hivyo vazi hilo ni najisi. Kuhani atalichoma moto vazi hilo kwani lina namna ya upele wa ukoma. “Kama kuhani ataona kuwa upele haukuenea katika vazi, basi, ataamuru vazi hilo lifuliwe na kuwekwa kando kwa muda mwingine wa siku saba. Kuhani ataliangalia hilo vazi baada ya kuoshwa. Ikiwa ile alama haijabadilika rangi yake hata ingawa upele haukuenea, basi, vazi hilo ni najisi. Vazi hilo utalichoma moto, iwe alama ya upele ipo nyuma au mbele ya vazi hilo. “Kama kuhani ataona kuwa ile alama imefifia baada ya kufuliwa, basi atararua ile sehemu iliyo na namna ya upele wa ukoma. Kisha, ikiwa hiyo alama inaonekana tena baadaye katika vazi lililofumwa au lililosokotwa au katika kitu chochote cha ngozi, basi upele umeenea. Hapo vazi hilo utalichoma moto. Lakini vazi ambalo upele umetokea baada ya kulifua itabidi lifuliwe mara ya pili na hivyo lipate kuwa safi.” Hiyo ni sheria kuhusu namna ya upele wa ukoma unaotokea katika vazi la sufu au kitani au lililofumwa au lililosokotwa au la ngozi. Kwa njia hiyo mtaweza kupambanua kati ya vazi lisilo najisi na lile lililo najisi. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Ifuatayo ni sheria kumhusu mwenye ukoma katika siku ya kutakaswa kwake. Baada ya kupona ataletwa kwa kuhani. Kuhani atakwenda kumwangalia huyo mtu nje ya kambi. Ikiwa ukoma huo umepona, basi, kuhani ataamuru watu walete ndege wawili safi walio hai, kipande cha mwerezi, sufu ya rangi nyekundu na tawi la husopo kwa ajili ya huyo mtu atakayetakaswa. Kuhani atawaamuru wamchinje ndege mmoja katika chungu chenye maji safi ya chemchemi. Kuhani atamchukua yule ndege mwingine hai, kipande kile cha mwerezi, sufu ya rangi nyekundu na lile tawi la husopo na kuvitumbukiza vyote katika damu ya yule ndege aliyechinjwa. Kisha, atamnyunyizia huyo mwenye kutakaswa ile damu mara saba, halafu atamtangaza mtu huyo kuwa safi. Yule ndege hai atamwacha aende zake mashambani nje ya mji. Huyo mtu atayafua mavazi yake, atanyoa nywele zake, na kuoga; naye atakuwa safi. Baada ya hayo atarudi kambini, lakini atakaa nje ya hema lake kwa muda wa siku saba. Siku ya saba atanyoa nywele zake zote, ndevu na kope za macho yake. Kisha atafua mavazi yake na kuoga, ataoga kwa maji; naye atakuwa safi. “Siku ya nane ataleta wanakondoo madume wawili wasio na dosari, kondoo jike wa mwaka mmoja asiye na dosari, kilo tatu za unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka pamoja na mafuta theluthi moja ya lita. Kuhani atakayemtakasa mtu huyo atamleta mbele ya Mwenyezi-Mungu karibu na mlango wa hema la mkutano pamoja na vitu alivyoleta. Kuhani atachukua mwanakondoo dume mmoja na kumtolea sadaka ya kuondoa hatia pamoja na yale mafuta theluthi moja ya lita. Atafanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kisha atamchinja huyo mwanakondoo katika mahali patakatifu, wanapochinjia wanyama wa sadaka ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuteketezwa. Sadaka hii ya kuondoa hatia, kama ilivyo sadaka ya kuondoa dhambi, ni mali yake kuhani; ni sadaka takatifu kabisa. Kuhani atachukua kiasi cha damu ya sadaka ya kuondoa hatia na kumpaka mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia na kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia. Kisha, kuhani atachukua kiasi cha ile theluthi moja ya mafuta na kuyatia katika kiganja cha mkono wake wa kushoto. Atachovya kidole cha mkono wake wa kulia katika mafuta hayo na kumnyunyizia huyo mtu anayetakaswa mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kiasi cha mafuta yanayobaki katika kiganja chake atampaka huyo mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia na kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia. Yale mafuta yaliyobaki atampaka huyo mtu kichwani. Hivyo kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kuhani atatolea sadaka ya kuondoa dhambi na kumfanyia huyo mtu anayetakaswa ibada ya upatanisho ili kumwondolea unajisi wake. Kisha atamchinja mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa. Kuhani atatolea ile sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka juu ya madhabahu. Hivyo kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho, naye atakuwa safi. “Lakini ikiwa mtu huyo ni maskini, hana uwezo wa kutoa vitu hivyo, basi ataleta mwanakondoo dume mmoja kuwa fidia ya sadaka ya kuondoa hatia ambaye atafanyiwa ishara ya kutoa sadaka ili kumfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho. Ataleta pia kilo moja ya unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka na mafuta theluthi moja ya lita. Ataleta pia hua wawili au makinda mawili ya njiwa kadiri anavyoweza mmoja atakuwa kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Siku ya nane atamletea kuhani vitu hivyo mbele ya mlango wa hema la mkutano kwa ajili ya utakaso wake mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kuhani atamchukua huyo mwanakondoo dume wa sadaka ya kuondoa hatia pamoja na yale mafuta theluthi moja ya lita na kufanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu. Atamchinja huyo mwanakondoo dume wa sadaka ya kuondoa hatia. Kuhani atachukua kiasi cha damu na kumpaka huyo mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia, katika kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia. Kuhani atatia kiasi cha mafuta hayo katika kiganja cha mkono wake wa kushoto. Kisha atamnyunyizia huyo mtu kwa kidole chake cha kulia kiasi cha hayo mafuta yaliyomo katika kiganja chake cha kushoto mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kuhani atampaka huyo mtu anayetakaswa mafuta katika ncha ya sikio lake la kulia, katika kidole gumba cha mkono wake wa kulia, na kidole gumba cha mguu wake wa kulia. Atampaka mahali pale ambapo alimpaka ile damu ya sadaka ya kuondoa hatia. Mafuta yanayosalia mkononi mwake atampaka huyo mtu kichwani, ili kumfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale hua au njiwa wawili kadiri mtu huyo anavyoweza kuleta. Hua atakuwa kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Pamoja na hao, atatoa sadaka ya nafaka; naye kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu. Huo ndio mwongozo kuhusu mtu mwenye ukoma asiyeweza kutoa sadaka za kumtakasa.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani ambayo ninawapa kuwa milki yenu, nami nikafanya namna ya upele wa ukoma uote katika ukuta wa nyumba fulani katika nchi mtakayoimiliki, basi, mwenye nyumba hiyo ni lazima amwambie kuhani kwamba namna ya upele wa ukoma umeonekana katika nyumba yake. Kuhani ataamuru vitu vyote ndani ya nyumba hiyo vitolewe kabla yeye mwenyewe hajaanza uchunguzi wake; visije vyote kutangazwa kuwa najisi. Kisha kuhani ataingia kuiangalia nyumba hiyo. Atauchunguza upele huo; kama upele huo umeonekana ukutani na umesababisha madoa ya rangi ya kijani kibichi au nyekundu na kuonekana kuwa yamepenya ndani ya kuta, basi, kuhani atatoka nje mlangoni na kuifunga nyumba hiyo kwa muda wa siku saba. Siku ya saba kuhani atarudi na kuiangalia tena nyumba hiyo. Ikiwa upele huo umeenea katika kuta za nyumba hiyo, kuhani ataamuru mawe yaliyoko kwenye sehemu zenye upele yatolewe na kutupwa mahali najisi nje ya mji. Lipu ya nyumba hiyo itabanduliwa na kifusi chake kutupwa mahali najisi nje ya mji. Kisha watachukua mawe mapya na kujenga mahali walipobomoa; nao wataipiga nyumba hiyo lipu upya. “Ikiwa upele huo utatokea tena baada ya kutoa mawe hayo na kukwangua lipu na kuipiga lipu upya, yapasa kuhani aje kuichunguza. Ikiwa upele umeenea katika nyumba hiyo, basi huo ni upele wa kufisha; nyumba hiyo ni najisi. Nyumba hiyo ni lazima ibomolewe na mawe yake, miti yake na lipu vipelekwe mahali najisi nje ya mji. Zaidi ya hayo, yeyote atakayeingia ndani ya nyumba hiyo wakati itakapokuwa imefungwa, atakuwa najisi mpaka jioni. Yeyote anayelala katika nyumba hiyo au kulia chakula ndani yake, lazima ayafue mavazi yake. “Lakini ikiwa baada ya kuikagua nyumba hiyo, kuhani ataona kuwa upele haujaenea baada ya kupigwa lipu, basi, kuhani atatangaza kuwa nyumba hiyo ni safi kwani upele umekwisha. Ili kuitakasa nyumba hiyo, mwenye nyumba ataleta ndege wawili pamoja na kipande cha mwerezi, sufu nyekundu na tawi la husopo. Atamchinja ndege mmoja katika chungu chenye maji safi ya chemchemi. Atachukua kipande cha mwerezi, tawi la husopo na ile sufu nyekundu pamoja na yule ndege mwingine aliye hai na kuvitumbukiza vyote katika damu ya yule ndege aliyechinjwa. Kisha atainyunyizia nyumba hiyo damu mara saba. Hivyo ndivyo atakavyoitakasa nyumba hiyo kwa damu ya ndege, maji safi ya chemchemi, ndege hai, kipande cha mwerezi, tawi la husopo na ile sufu nyekundu. Yule ndege hai atamwacha aende zake mashambani nje ya mji. Hivyo ndivyo atakavyoitakasa nyumba hiyo, nayo itakuwa safi.” Hii ndiyo sheria kuhusu aina yoyote ya namna ya upele wa ukoma; upele katika nguo au nyumba, uvimbe, jipu au kipaku, ili kuonesha ni kitu gani kilicho najisi na kisicho najisi. Hiyo ndiyo sheria kuhusu namna ya upele wa ukoma. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose na Aroni, “Waambieni Waisraeli hivi: Mwanamume yeyote akitokwa na usaha, usaha huo wamfanya kuwa najisi. Na ufuatao ni mwongozo kuhusu najisi hiyo: Muda wote anapotokwa na usaha au usaha unapokuwa umezuiwa ndani yake, mtu huyo ni najisi. Kitanda chochote atakacholalia au atakachokalia, kitakuwa najisi. Mtu yeyote atakayegusa kitanda chake mtu huyo ni lazima ayafue mavazi yake, na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni. Mtu yeyote atakayekalia kitu chochote alichokalia huyo mtu mwenye kutokwa na usaha, ni lazima ayafue mavazi na kuoga; na atakuwa najisi hadi jioni. Mtu yeyote atakayemgusa mtu atokwaye na usaha, lazima afue mavazi yake na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni. Mtu yeyote akitemewa mate na mtu anayetokwa usaha ni lazima mtu huyo aliyetemewa mate ayafue mavazi yake, na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni. Tandiko lolote la mnyama aliloketia mtu anayetokwa na usaha litakuwa najisi. Mtu yeyote atakayegusa kitu chochote alichokalia mtu huyo, atakuwa najisi mpaka jioni. Mtu yeyote anayebeba kitu chochote kilichokuwa cha mtu huyo ni lazima ayafue mavazi yake, na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni. Mtu yeyote anayetokwa na usaha akimgusa mtu bila kusafisha kwanza mikono yake na kuoga, aliyeguswa atakuwa najisi mpaka jioni. Chombo chochote cha udongo kilichoguswa na mtu anayetokwa na usaha ni lazima kivunjwe. Lakini chombo chochote cha mbao ni lazima kisafishwe kwa maji. “Mwanamume yeyote anayetokwa na usaha akiponywa ugonjwa wake, ni lazima huyo mtu angoje siku saba kabla ya kuondolewa unajisi wake. Atayafua mavazi yake na kuoga kwa maji ya mtoni; naye atakuwa safi. Siku ya nane, ni lazima alete hua wawili au makinda mawili ya njiwa mbele ya Mwenyezi-Mungu mlangoni mwa hema la mkutano na kumkabidhi kuhani. Kuhani atawatoa hao, mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumwondolea unajisi wake wa kutokwa na usaha. “Kama mwanamume yeyote akitokwa na shahawa yake, ni lazima aoge mwili mzima kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni. Vazi lolote lililodondokewa shahawa au ngozi yoyote iliyoguswa na shahawa hiyo ni lazima ioshwe kwa maji, na itakuwa najisi mpaka jioni. Kama mwanamume akilala na mwanamke, akatokwa na shahawa, basi, ni lazima wote wawili waoge kwa maji, nao watakuwa najisi mpaka jioni. “Mwanamke yeyote anapokuwa mwezini, atakuwa najisi kwa muda wa siku saba. Mtu yeyote atakayemgusa mwanamke huyo atakuwa najisi mpaka jioni. Kitu chochote anacholalia au kukalia wakati yu najisi, kitakuwa najisi. Mtu yeyote atakayegusa kitanda cha huyo mwanamke ni lazima ayafue mavazi yake na kuoga kwa maji; naye atakuwa najisi mpaka jioni. Mtu yeyote atakayegusa kitu chochote anachokalia mwanamke huyo ni lazima ayafue mavazi yake na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni. Mwanamume yeyote atakayegusa kitu chochote alicholalia au kukalia huyo mwanamke, atakuwa najisi mpaka jioni. Kama mwanamume akilala na mwanamke huyo na damu ya huyo mwanamke ikamdondokea huyo mwanamume, basi, mwanamume huyo atakuwa najisi kwa muda wa siku saba. Kitanda chochote atakacholalia huyo mwanamume kitakuwa najisi. “Kama mwanamke anatokwa na damu kwa muda wa siku nyingi kuliko ilivyo kawaida au anatokwa damu wakati usio wa majira yake ya kutokwa damu, basi, ataendelea kuwa najisi muda wote damu inapomtoka. Kitanda chochote anacholalia wakati huo au kiti chochote anachokalia, kitakuwa najisi sawa kama wakati wa unajisi wake wa kutokwa damu. Mtu yeyote atakayegusa vitu hivyo, atakuwa najisi na ni lazima ayafue mavazi yake na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni. Baada ya kukauka damu yake mwanamke huyo atangoja hadi siku saba ili kuwa safi; na baada ya muda huo atakuwa safi. Siku ya nane atachukua hua wawili au makinda mawili ya njiwa na kumletea kuhani mlangoni mwa hema la mkutano. Kuhani atamtoa mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Hivyo kuhani atamfanyia huyo mwanamke ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumwondolea unajisi wake wa kutokwa damu. “Ndivyo mtakavyowatahadharisha Waisraeli na unajisi wao, wasije wakaikufuru maskani yangu takatifu iliyo miongoni mwao wakiingia humo na unajisi wao; wakifanya hivyo watauawa.” Hiyo ndiyo sheria kuhusu mwanamume anayetokwa na usaha na anayetokwa na shahawa na kuwa najisi. Sheria hiyo yamhusu pia mwanamke anayetokwa damu na kuwa najisi. Sheria hiyo yamhusu mwanamume au mwanamke yeyote anayetokwa na chochote na pia yahusu mwanamume anayelala na mwanamke ambaye ni najisi. Mwenyezi-Mungu alizungumza na Mose, baada ya wana wawili wa Aroni kufa wakati ule walipomkaribia. Alimwambia, “Mwambie ndugu yako Aroni asiingie mahali patakatifu nyuma ya pazia wakati usiokubaliwa. Asiingie mahali hapo kwani ndipo nitakapotokea katika wingu juu ya kiti cha rehema. Asipotii, atakufa. Aroni ataingia mahali patakatifu sana akiwa na fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Ataoga mwili wote katika maji, kisha atavaa mavazi matakatifu. Ataingia mahali hapo akiwa amevaa mavazi matakatifu: Joho la kitani baada ya nguo ya ndani ya suruali ya kitani na akiwa amevaa kanzu ya kitani na kujifunga mkanda wa kitani. Atatwaa kutoka jumuiya ya watu wa Israeli beberu wawili kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na kondoo dume mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. “Aroni atamtoa huyo fahali sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili yake mwenyewe, na kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na jamaa yake. Kisha, wale beberu wawili atawaweka kwenye mlango wa hema la mkutano. Atawapigia kura hao beberu wawili, kura moja kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na nyingine kwa ajili ya Azazeli. Atamleta yule beberu ambaye kura ilimtaka kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kumtolea sadaka ya kuondoa dhambi. Lakini yule beberu aliyetakiwa na kura kwa ajili ya Azazeli atatolewa mbele ya Mwenyezi-Mungu akiwa hai ili kufanya ibada ya upatanisho kuhani atamwacha aende jangwani kwa Azazeli, ili kuondoa dhambi za jumuiya. “Aroni atamtoa fahali wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili yake mwenyewe, na kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya jamaa yake, kisha atamchinja fahali huyo sadaka ya kuondoa dhambi. Halafu atachukua chetezo na kutwaa makaa madhabahuni mbele ya Mwenyezi-Mungu na ubani konzi mbili uliosagwa vizuri sana. Ili asije akafa, atauleta ubani huo mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuutia katika moto ili moshi wa ubani huo ukifunike kifuniko cha sanduku la agano. Atachukua kiasi cha damu ya yule fahali na kunyunyiza kwa kidole chake upande wa mashariki juu ya kiti cha rehema kisha atainyunyizia mbele ya sanduku la agano mara saba kwa kidole chake. “Halafu atamchinja yule beberu wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya watu wote. Damu ya mbuzi huyo ataileta ndani mahali patakatifu sana na kufanya kama alivyofanya na damu ya yule fahali; atainyunyiza juu ya kiti cha rehema, upande wake wa mbele. Hivyo atafanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu kwa sababu ya unajisi, makosa na dhambi zote za Waisraeli. Ndivyo atakavyofanya pia kwa ajili ya hema la mkutano lililo miongoni mwa watu hao walio najisi. Wakati Aroni anafanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, jamaa yake na jamii nzima ya Israeli, kamwe asiwepo mtu yeyote ndani ya hema la mkutano hadi atakapokuwa amemaliza na kutoka nje. Kisha atatoka na kwenda kwenye madhabahu iliyo mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuifanyia ibada ya upatanisho. Atachukua kiasi cha damu ya yule fahali na ya yule mbuzi na kuzipaka pembe za madhabahu pande zote. Atainyunyizia madhabahu hiyo damu kwa kidole chake mara saba na hivyo kuiweka wakfu na kuitakasa unajisi wote wa watu wa Israeli. “Baada ya Aroni kumaliza kupatakasa mahali patakatifu, hema la mkutano na madhabahu, ndipo atamtoa yule beberu kwa ajili ya Azazeli, akiwa hai. Aroni ataweka mikono yake juu ya kichwa cha huyo beberu hai na kuuungama juu yake dhambi zote za watu wa Israeli, makosa yao yote na dhambi zao zote, ili kumwajibisha huyo. Kisha atamwacha huyo beberu aende jangwani akipelekwa huko na mtu yeyote anayejitoa kwa hiari. Atamwacha huyo beberu aende jangwani, mahali pasipokuwa na watu, akiwa ameyachukua maovu yao yote. “Kisha Aroni atarudi ndani ya hema la mkutano, atavua yale mavazi aliyovaa alipoingia mahali patakatifu sana na kuyaacha humo. Ataoga humo ndani katika mahali patakatifu na kuvaa mavazi yake. Atatoka na kutoa sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka ya kuteketezwa ya watu wa Israeli, ili kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote. Mafuta ya sadaka ya kuondoa dhambi atayateketeza juu ya madhabahu. Yule mtu aliyempeleka yule beberu kwa Azazeli kwanza atayafua mavazi yake na kuoga ndipo atakapoweza kuingia kambini. Yule fahali na mbuzi waliotolewa sadaka ya kuondoa dhambi ambao damu yao ilipelekwa mahali patakatifu sana ili kufanya ibada ya upatanisho, watapelekwa nje ya kambi na kuteketezwa. Ngozi zao, nyama na mavi yao, vyote vitateketezwa. Yule mtu atakayewateketeza atayafua mavazi yake na kuoga, ndipo atakapoweza kuingia kambini. “Hili ni sharti ambalo mnapaswa kulifuata milele: Siku ya kumi ya mwezi wa saba, nyinyi wenyewe na hata wageni wanaoishi miongoni mwenu, ni lazima mfunge siku hiyo na kuacha kufanya kazi. Mtafanya hivyo kwa sababu siku hiyo ndiyo siku ambayo mtafanyiwa ibada ya upatanisho, msafishwe dhambi zenu, nanyi mtakuwa safi mbele ya Mwenyezi-Mungu. Siku hiyo ni siku ya mapumziko kamili nanyi mtafunga. Kanuni hiyo ni ya kudumu milele. Kuhani aliyepakwa mafuta na kuwekwa wakfu ashike nafasi ya baba yake, ndiye atakayefanya ibada ya upatanisho akiwa amevaa mavazi matakatifu ya kitani. Atafanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu sana, kwa ajili ya hema la mkutano, madhabahu, makuhani na kwa ajili ya jumuiya nzima ya Israeli. Hili, basi ni sharti la kudumu milele; ni lazima mlifuate ili kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya watu wa Israeli mara moja kila mwaka na kusamehewa dhambi zao.” Mose akafanya yote kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mwambie Aroni, wanawe na watu wote wa Israeli amri zifuatazo: Kama mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli akichinja ng'ombe au mwanakondoo au mbuzi ndani au nje ya kambi, badala ya kumleta mnyama huyo kwenye mlango wa hema la mkutano ili kumtolea Mwenyezi-Mungu mbele ya maskani yake takatifu, mtu huyo atakuwa na hatia ya kumwaga damu; amemwaga damu na atatengwa na watu wake. Kusudi la sheria hii ni kwamba Waisraeli wanapaswa kuleta wanyama ambao wangewachinjia mashambani ili wawalete kwa Mwenyezi-Mungu kwa kuhani kwenye mlango wa hema la mkutano, naye atawachinja na kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za amani. Basi, kuhani atainyunyizia damu madhabahu ya Mwenyezi-Mungu iliyoko mlangoni mwa hema la mkutano na kuyateketeza yale mafuta yawe harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Kwa hiyo Waisraeli watakoma kabisa kutambikia yale majini, jambo ambalo limewafanya wakose uaminifu kwangu. Sharti hili ni la kudumu milele katika vizazi vyao vyote. “Waambie kwamba mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli au mgeni anayeishi kati yao, anayetoa sadaka ya kuteketezwa au tambiko, lakini haileti mbele ya mlango wa hema la mkutano ili kumtolea Mwenyezi-Mungu, mtu huyo atatengwa na watu wake. “Kama mtu yeyote wa jumuiya ya Israeli au mgeni anayeishi kati yao anakula damu yoyote, mimi nitamwandama mtu huyo aliyekula damu na kumtenga mbali na watu wake. Itakuwa hivyo kwa sababu uhai wa kiumbe umo katika damu. Nimewaagiza kuitolea damu madhabahuni ili kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya roho zenu; kwa sababu damu hufanya upatanisho maana uhai umo katika damu. Ndiyo maana nimewaagiza Waisraeli hivi: Mtu yeyote miongoni mwenu wala mgeni anayeishi kati yenu kamwe asile damu. “Mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli au mgeni anayekaa miongoni mwao akienda kuwinda mnyama au ndege, ni lazima aimwage damu chini na kuifunika kwa udongo. Maana, uhai wa kila kiumbe umo katika damu. Ndiyo maana nimewaagiza Waisraeli, kamwe wasile damu ya kiumbe chochote kwani uhai wa kiumbe chochote ni damu yake. Yeyote atakayekula damu atatengwa. “Mtu yeyote awe ni mwenyeji au mgeni, anayekula chochote kilichokufa chenyewe au kilichouawa na mnyama wa porini, lazima ayafue mavazi yake na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni. Baada ya hapo atakuwa safi. Lakini asipoyafua mavazi yake na kuoga, ni lazima mtu huyo awajibike kwa uovu wake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie watu wa Israeli hivi: Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kamwe msifanye kama wafanyavyo watu wa nchi ya Misri ambako mlikaa; wala msifanye kama wafanyavyo watu wa nchi ya Kanaani ambako nawapeleka. Kamwe msifuate mitindo yao. Nyinyi mtafuata maagizo yangu na kuyashika masharti yangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kwa hiyo, ili mtu apate kuyaokoa maisha, mnapaswa kuyashika masharti yangu na maagizo yangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Mtu yeyote wa Israeli haruhusiwi kumkaribia mtu wa jamaa yake wa karibu ili kulala naye. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. Kamwe usimvunjie heshima baba yako kwa kulala na mama yako aliyekuzaa. Usimwaibishe; yeye ni mama yako. Kamwe usimvunjie heshima baba yako kwa kulala na mmoja wa wake zake. Hao ni mama zako. Kamwe usilale na dada yako, awe ni dada yako halisi au dada yako wa kambo. Kamwe usilale na mjukuu wako, mtoto wa mwanao au binti yako; maana sehemu zao za siri ni kama zako mwenyewe. Kamwe usilale na msichana aliyezaliwa na mama yako wa kambo aliyeolewa na baba yako; msichana huyo ni dada yako. Kamwe usilale na shangazi yako; kwani huyo ni dada wa baba yako. Kamwe usilale na dada wa mama yako; kwani huyo ni mama yako mkubwa au mdogo. Kamwe usilale na mke wa baba yako mkubwa au mdogo; huyo ni mama yako. Kamwe usilale na mke wa mwanao; huyo ni mkewe mwanao. Kamwe usilale naye. Kamwe usilale na mke wa ndugu yako; huyo ni shemeji yako. Ukilala na mwanamke, basi, kamwe usilale naye na binti yake, wala wajukuu zake. Hao ni ndugu. Kuwachanganya ni kufanya uovu. Kamwe usimwoe dada wa mkeo wakati mke wako yungali hai; hiyo itasababisha ushindani. “Kamwe usilale na mwanamke awapo mwezini. Kamwe usilale na mke wa jirani yako na hivyo kujitia mwenyewe najisi naye. “Kamwe usimtoe mtoto wako yeyote kuwa sadaka kwa mungu Moleki maana kufanya hivyo utalikufuru jina langu mimi Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Kamwe usilale na mwanamume mwenzio kana kwamba ni mwanamke. Hilo ni chukizo. Kamwe usilale na mnyama ili usijitie najisi; mwanamume au mwanamke yeyote kamwe asifanye hivyo; kufanya hivyo ni upotovu. “Msijitie najisi kwa kufanya mambo hayo kwani kwa sababu ya mambo hayo nayafukuza mataifa yaliyo mbele yenu kwa vile wao hufanya hayo na kujitia najisi. Nchi yao ilitiwa unajisi nami nikaiadhibu, nayo ikawakataa wakazi wake. Lakini nyinyi na wageni wanaokaa kati yenu ni lazima kuyashika masharti na maagizo yangu na wala msifanye machukizo hayo. Machukizo hayo waliyafanya watu waliokaa katika nchi ya Kanaani kabla yenu, nao wakaitia nchi unajisi. Basi, nyinyi msifanye mambo hayo, la sivyo nchi hiyo itawatapika kama ilivyolitapika taifa lililokuwa kabla yenu. Watu wote watakaofanya mambo hayo ya kuchukiza ni lazima watengwe mbali na watu wao. Kwa hiyo shikeni kikamilifu yote ninayowaagiza; msifuate mazoea yoyote ya kuchukiza yaliyofanywa na wale walioishi nchini kabla yenu, msije mkajitia unajisi kwayo. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Iambie jumuiya yote ya watu wa Israeli hivi: Ni lazima muwe watakatifu kwani mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni mtakatifu. Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Msizigeukie sanamu za miungu, wala msijitengenezee sanamu za kusubu za miungu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Mnaponitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za amani, mtanitolea kama itakiwavyo ili mpate kukubaliwa. Sadaka hiyo ni lazima iliwe siku hiyohiyo inapotolewa au kesho yake. Chochote kinachobaki hadi siku ya tatu ni lazima kiteketezwe kwa moto. Kama sehemu ya nyama yake italiwa siku ya tatu, tendo hilo ni chukizo; na sadaka hiyo haitakubaliwa, naye atakayekula nyama hiyo ni lazima awajibike kwa uovu wake kwa sababu amekitia unajisi kitu kitakatifu cha Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo atatengwa na watu wake. “Utakapovuna mavuno ya nchi yako, usivune kabisa hadi mpakani mwa shamba wala usirudi nyuma kukusanya mabaki. Msirudie kukusanya kila kitu katika shamba la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini; utawaachia maskini na wageni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Msiibe, msidanganye wala kuambiana uongo. Msiape uongo kwa jina langu hata kulikufuru jina la Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Usimdhulumu jirani yako wala kumwibia. Mshahara wa mtu aliyeajiriwa usikae kwako usiku kucha hadi asubuhi. Usimlaani kiziwi wala kuweka kizuizi mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Unapotoa hukumu uamue kwa haki; usimpendelee maskini wala kumwogopa mwenye cheo. Bali ni lazima kumwamua jirani kwa haki. Kamwe usipitepite ukiwachongea watu wa jamaa yako. Usiyatie maisha ya jirani yako katika hatari ya kifo kwa maneno yako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Usimwekee kisasi ndugu yako moyoni mwako, bali upatane daima na jirani yako ili usije ukatenda dhambi. Usijilipize kisasi au kuwa na kinyongo dhidi ya wazawa wa watu wako bali umpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Yakupasa kuyashika masharti yangu. Usiiache mifugo yako ipandwe na wanyama wa aina nyingine. Shambani mwako usipande mbegu za aina mbili. Usivae vazi lililofumwa kwa aina mbili za nguo. “Mwanamume akilala na mwanamke mtumwa ambaye ameposwa na mwanamume mwingine, lakini bado hajakombolewa wala kupewa uhuru, uchunguzi ufanywe. Lakini wasiuawe kwa sababu mwanamke huyo hakuwa bado huru. Mwanamume huyo ataleta mbele ya hema la mkutano sadaka yake ya kondoo dume ya kuondoa hatia na kunitolea mimi Mwenyezi-Mungu. Kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho kwa kutumia kondoo huyo mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya dhambi aliyotenda; naye atasamehewa dhambi hiyo aliyotenda. “Mtakapofika katika nchi ya Kanaani na kupanda aina zote za miti ya matunda, matunda hayo hamtayala; hamtaruhusiwa kuyala kwa muda wa miaka mitatu. Mnamo mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa matakatifu, yatatolewa kuwa sadaka ya sifa, kwa Mwenyezi-Mungu. Lakini matunda ya kuanzia mwaka wa tano hayo mnaweza kula, na mavuno yenu yataongezeka. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Msile nyama yoyote yenye damu. Msipige bao wala kufanya uchawi. Nywele zenu msizikate pembeni wala kunyoa ndevu zenu. Msijitie alama zozote mwilini mwenu kwa ajili ya kuomboleza au kujikatakata mwilini au kujichanja chale. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Usimchafue binti yako kwa kumfanya kahaba, nchi nzima isije ikaangukia katika ukahaba na hivyo kujaa uovu. Mtazishika Sabato zangu na kupaheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Msiwaendee waaguzi wa mizimu wala wachawi ili kuwaomba wawaagulie na hivyo mkajitia najisi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Uwapo mbele ya mzee ni lazima usimame ili kumpa heshima yake; nawe umche Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Kama kuna mgeni katika nchi yako usimtendee vibaya. Huyo mgeni anayekaa nawe atakuwa kwako kama mwenyeji nawe utampenda kama unavyojipenda mwenyewe, kwa kuwa nawe ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Usikose kamwe kuamua kwa haki kuhusu vipimo vya urefu, uzito na ujazo. Ni lazima mtumie mizani halali, na vipimo vilivyo halali. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri. Ni lazima kuyashika na kuyatekeleza masharti yangu na maagizo yangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli au mgeni anayekaa miongoni mwenu, akimtoa sadaka mtoto wake yeyote kwa mungu Moleki ni lazima mtu huyo auawe. Wananchi wa hapo watamuua kwa kumpiga mawe. Mimi mwenyewe nitamkabili mtu huyo na kumtenga na watu wake kwa sababu alimtoa mmoja wa watoto wake sadaka kwa mungu Moleki na hivyo kupachafua mahali pangu patakatifu na jina langu takatifu. Kama wananchi wa mahali hapo hawatamwadhibu mtu huyo kwa kumuua, mimi mwenyewe nitamkabili mtu huyo na jamaa yake. Nitawatenga kutoka watu wao, yeye mwenyewe pamoja na wote waliokosa uaminifu kwangu kwa kumwendea mungu Moleki. “Kama mtu yeyote anawaendea waaguzi wa mizimu na wachawi na hivyo kukosa uaminifu kwangu, nitamkabili mtu huyo na kumtenga na watu wake. Kwa hiyo, jiwekeni wakfu muwe watakatifu; kwani mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Shikeni masharti yangu na kuyatekeleza. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu ninayewatakasa. Mtu yeyote amlaaniye baba yake au mama yake, ni lazima auawe. Amemlaani baba au mama yake, kwa hiyo damu yake itakuwa juu yake. “Kama mwanamume akizini na mke wa jirani yake, ni lazima wote wawili wauawe. Mwanamume akilala na mmoja wa wake za baba yake, anamwaibisha baba yake; wote wawili ni lazima wauawe. Damu yao itakuwa juu yao wenyewe. Mwanamume yeyote akilala na mke wa mwanawe, wote wawili ni lazima wauawe. Wamefanya zinaa ya maharimu; wanawajibika kwa umwagaji wa damu yao wenyewe. Kama mwanamume yeyote akilala na mwanamume mwenzake kana kwamba ni mwanamke, basi, wote wawili ni lazima wauawe kwani wamefanya jambo lililo chukizo; watawajibika kwa umwagaji wa damu yao wenyewe. Kama mwanamume akioa mke na pia kumwoa mama yake, huo ni uovu; wote watatu ni lazima wateketezwe kwa moto kwani wamefanya uovu. Mtafanya hivyo ili uovu usiwe miongoni mwenu. Kama mwanamume yeyote akilala na mnyama ni lazima auawe; na mnyama huyo lazima auawe. Kama mwanamke akimkaribia mnyama na kulala naye ni lazima mwanamke huyo auawe na mnyama huyo pia; damu yao itakuwa juu yao wenyewe. “Kama mwanamume yeyote akimwoa dada yake, binti ya baba yake au mama yake, na binti huyo akakubaliana na mwanamume huyo ambaye ni kaka yake, na kulala naye, hilo ni chukizo, ni lazima watengwe na rika lao kwani wamefanya jambo la aibu. Ni lazima mwanamume huyo awajibike kwa uovu wake. Kama mwanamume akilala na mwanamke aliye mwezini, wote wawili ni lazima watengwe na watu wao; huyo mwanamume amelala na mwanamke aliye na hedhi, na huyo mwanamke amelala na mwanamume akiwa na hedhi. Usilale na dada ya mama yako wala na shangazi yako, maana hao ni jamaa yako wa karibu. Wote watendao hayo watawajibika kwa uovu wao. Kama mtu akilala na mke wa baba yake, mkubwa au mdogo, anamwaibisha baba yake mkubwa au mdogo; wote wawili watawajibika kwa dhambi yao; wote wawili watakufa bila watoto. Kama mwanamume akimwoa mke wa ndugu yake, anamwaibisha ndugu yake, huo ni unajisi; wote wawili watakufa bila watoto. “Mnapaswa kushika na kutekeleza masharti na maagizo yangu yote; la sivyo nchi ile ambamo ninawapeleka itawatapika. Msizifuate desturi za taifa ninalolifukuza mbele yenu; kwani waliyafanya hayo yote, nami nikawachukia sana. Lakini, nimekwisha waambia, ‘Mtarithi nchi yao, mimi nawapa nchi hiyo muimiliki, nchi inayotiririka maziwa na asali.’ Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu niliyewatenga na mataifa mengine. Kwa hiyo, ni lazima mtofautishe kati ya mnyama asiye najisi na aliye najisi, kati ya ndege asiye najisi na aliye najisi. Msijifanye kuwa najisi kwa kugusa mnyama au ndege au chochote kitambaacho duniani ambacho nimekitenga kuwa ni najisi. Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ni mtakatifu, nami nimewatenga nyinyi na mataifa mengine ili muwe mali yangu, mtakuwa watakatifu. “Mwanamume au mwanamke yeyote aliye mlozi au mchawi, ni lazima auawe kwa kupigwa mawe. Wote watawajibika kwa umwagaji wa damu yao wenyewe.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie makuhani, wana wa Aroni, kwamba pasiwe na mtu yeyote miongoni mwao atakayejitia najisi kwa kugusa maiti ya watu wa jamaa yake, isipokuwa kama ni maiti ya ndugu yake wa karibu, yaani mama yake, baba yake, mwanawe, binti yake, ndugu yake au dada yake ambaye (aliye wa jamaa yake ya karibu), naye hajaolewa bado. Yeye, akiwa mwenye madaraka katika jamaa yake, asijitie unajisi. Wazawa wa Aroni kamwe wasijinyoe upara kuomboleza wala wasikate pembe za ndevu zao wala kujichanja chale mwilini. Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao wala wasilikufuru jina la Mungu wao. Maana wao ndio wanaotolea zile sadaka anazopewa Mwenyezi-Mungu kwa moto yaani chakula cha Mungu. Basi, ni lazima wawe watakatifu. Kwa kuwa kuhani amewekwa wakfu kwa Mungu wake, kamwe asioe kahaba, wala mwanamke asiye bikira wala aliyepewa talaka. Utamtambua kuhani kuwa aliyewekwa wakfu, maana yeye ndiye anayetoa sadaka ya mkate wa Mungu wako; utamtambua kuwa mtakatifu, maana mimi Mwenyezi-Mungu ninayekuweka wewe wakfu, ni mtakatifu. Binti wa kuhani yeyote akijitia unajisi kwa kufanya ukahaba, atateketezwa kwa moto kwani anamtia baba yake unajisi. “Kuhani mkuu yeyote, kwa kuwa yeye ni mkuu kati ya ndugu zake, naye amemiminiwa mafuta ya kupaka kichwani pake, na kuwekwa wakfu ili ayavae mavazi matakatifu, asiache nywele zake kuwa ovyo wala asirarue mavazi yake kuomboleza. Asikaribie maiti wala kujitia unajisi kwa maiti hata kama ni ya baba yake au ya mama yake. Kwa kuwa amewekwa wakfu kwa kupakwa mafuta ya Mungu wake kichwani, basi asiondoke mahali patakatifu wala asipatie unajisi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. Kuhani mkuu aweza tu kumwoa msichana ambaye ni bikira. Haruhusiwi kuoa mwanamke mjane, mwanamke asiye bikira, wala kahaba. Ni lazima aoe bikira kutoka watu wake mwenyewe asije akawatia unajisi watoto wake mwenyewe. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu niliyemweka wakfu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mwambie Aroni hivi: Mzawa wako yeyote katika vizazi vyote vijavyo ambaye ana dosari mwilini, haruhusiwi kukaribia na kunitolea mimi Mungu wake sadaka ya mkate. Mtu yeyote mwenye dosari sikaribie kunitolea sadaka: Awe kipofu, aliyelemaa, aliyeharibika uso, mwenye kiungo kirefu kuliko kawaida, mwenye mguu au mkono ulioumia, mwenye kibyongo, mtu mfupi kuliko kawaida, mwenye macho mabovu au ugonjwa wa ngozi, mwenye upele au towashi. Mzawa yeyote wa kuhani Aroni mwenye kilema asikaribie kunitolea sadaka za kuteketezwa kwa moto; kwa vile ana kilema, basi, asikaribie kunitolea mimi Mungu mkate wangu. Mtu huyo anaweza kula mkate wa Mungu wake, vitu vitakatifu na vile vitakatifu kabisa. Lakini asilikaribie lile pazia wala ile madhabahu kwani ana dosari, asije akapatia unajisi mahali patakatifu; kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayewaweka wakfu.” Mose akamweleza Aroni na wanawe na Waisraeli wote mambo hayo yote. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mwambie Aroni na wanawe makuhani waviheshimu vitu ambavyo Waisraeli wameniwekea wakfu, wasije wakalikufuru jina langu takatifu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. Waambie hivi: Kama mmoja wa wazawa wenu katika vizazi vyenu vyote atavikaribia vitu vitakatifu ambavyo Waisraeli wameviweka wakfu kwangu mimi Mwenyezi-Mungu akiwa najisi, mtu huyo atatengwa nami. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. Mtu yeyote wa nasaba ya Aroni akiwa na ugonjwa wa ukoma au anatokwa usaha asile vitu vitakatifu mpaka atakapokuwa safi. Mtu yeyote akimgusa mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti au mtu aliyetokwa na shahawa, au akigusa kiumbe chochote chenye kutambaa ambacho husababisha mtu kuwa najisi au mtu ambaye aweza kumtia unajisi wa aina yoyote ile, mtu huyo, atakuwa najisi mpaka jioni na haruhusiwi kula vyakula vitakatifu mpaka hapo atakapokuwa ameoga. Jua litakapotua ndipo atakapokuwa safi. Baada ya hapo ataweza kula vyakula vitakatifu kwani hicho ndicho chakula chake. Kuhani asile nyama yoyote ya mnyama aliyekufa peke yake au kuuawa na mnyama wa porini, asije akajitia unajisi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. Kwa hiyo, ni lazima makuhani walishike agizo langu, wasije wakafanya dhambi na kuuawa. Mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayewaweka wakfu. “Mtu asiye wa ukoo wa makuhani haruhusiwi kula chakula kitakatifu. Hata mgeni wa kuhani au mwajiriwa wake haruhusiwi kula. Lakini kama kuhani amemnunua mtumwa ili kuwa mali yake, basi, huyo mtumwa anaruhusiwa kula na pia wale waliozaliwa nyumbani kwake. Kama binti yake kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, haruhusiwi kula sadaka ya vitu vitakatifu. Lakini kama binti yake kuhani ni mjane au amepewa talaka na hana mtoto, naye amerudi nyumbani kwa baba yake, akakaa naye kama alipokuwa kijana, basi, anaweza kula chakula cha baba yake. Hata hivyo, mgeni haruhusiwi kula vyakula hivyo. Kama mtu mwingine akila vyakula vitakatifu bila kujua, basi, atalipa asilimia ishirini ya thamani ya alichokula na kumrudishia kuhani. Kuhani asivitie unajisi vitu ambavyo Waisraeli wamemtolea Mwenyezi-Mungu na hivyo kusababisha watu wawajibike uovu na hatia yao kwa kula vitu vyao vitakatifu. Mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayeviweka wakfu vitu hivyo.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mwambie Aroni na wanawe makuhani na Waisraeli wote hivi: Kama mtu yeyote miongoni mwenu au mgeni yeyote aishiye katika Israeli akitoa sadaka yake, iwe ni ya kutimiza nadhiri au sadaka ya hiari ya kumtolea Mwenyezi-Mungu kwa kuteketezwa, ili apate kukubalika, atatoa katika ng'ombe dume au katika kondoo dume asiye na dosari. Ni marufuku kutoa chochote kilicho na dosari kwani hakitakubaliwa kwa faida yenu. Mtu yeyote anapomtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya amani ili kutimiza nadhiri au sadaka ya hiari kutoka katika kundi lake la mifugo, ili akubaliwe ni lazima awe ni mnyama mkamilifu; mnyama huyo asiwe na dosari yoyote. Usimtolee Mwenyezi-Mungu mnyama yeyote aliye kipofu, kilema, aliyevunjika mahali, anayetokwa na usaha, mwenye upele au ukurutu, wala usiwatoe kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu. Fahali au mwanakondoo aliye na kiungo kimoja kirefu au kifupi kuliko kawaida waweza kumtoa sadaka ya hiari; lakini huyo usimtoe kuwa sadaka ya kutimiza nadhiri. Mnyama ambaye kiungo chake cha kiume kimejeruhiwa, kimepondwa, kimevunjwa au kimekatwa, kamwe usimtolee Mwenyezi-Mungu; usifanye kitu cha namna hiyo nchini mwako. Wala usipokee kutoka kwa wageni wanyama wa namna hiyo na kunitolea mimi Mungu wako kama chakula. Wanyama hao wana dosari kwa vile wamekatwa na hawatakubaliwa kwa faida yenu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Fahali, kondoo dume au beberu akizaliwa atabaki na mama yake kwa siku saba. Lakini tangu siku ya nane anaweza kutolewa kwa Mwenyezi-Mungu kama sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Lakini usimchinje ng'ombe au kondoo siku moja pamoja na ndama wake. Utakaponitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya shukrani utaitoa kwa namna ambayo itakufanya ukubaliwe. Mnyama huyo ni lazima aliwe siku hiyohiyo; msimbakize mpaka kesho yake asubuhi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Kwa hiyo mtazishika na kuzitekeleza amri zangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. Msilikufuru jina langu takatifu, kwani ni lazima niheshimiwe miongoni mwa watu wa Israeli. Mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayewaweka wakfu. Mimi ndimi niliyewatoa nchini Misri ili niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Katika sikukuu zangu mimi Mwenyezi-Mungu ambazo zimepangwa mtakuwa na mkutano mtakatifu. Sikukuu ambazo nimepanga ni hizi: Kutakuwa na siku sita za kufanya kazi. Lakini siku ya saba ni Sabato; siku hiyo ni ya mapumziko rasmi, hamtafanya kazi na mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo ya saba hamtafanya kazi; hiyo ni Sabato ambayo ni wakfu kwangu mimi Mwenyezi-Mungu katika makao yenu yote. “Sikukuu zangu nyingine mimi Mwenyezi-Mungu ambazo mtakuwa na mkutano mtakatifu zitafanyika katika nyakati zifuatazo zilizopangwa. “Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza mtaadhimisha kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu sikukuu ya Pasaka. Siku ya kumi na tano ya mwezi huohuo, sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu itaanza. Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo msifanye kazi. Kwa muda wa siku hizo zote saba mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa kwa moto. Katika siku ya saba mtafanya mkutano mtakatifu. Msifanye kazi.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Mtakapoingia katika nchi ambayo ninawapeni mkavuna mazao yake, mtamletea kuhani mganda wa mavuno ya kwanza. Kuhani atafanya nayo ishara ya kunitolea siku inayofuata siku ya Sabato ili mpate kukubaliwa. Siku hiyo mnapofanya ishara ya kutoa huo mganda mbele yangu mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa ya mwanakondoo dume wa mwaka mmoja asiye na dosari. Pamoja na sadaka hiyo, mtatoa sadaka ya nafaka ya kilo mbili za unga laini uliochanganywa na mafuta ambayo mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu kwa moto, na harufu yake itanipendeza. Sadaka yake ya kinywaji ni lita moja ya divai. Kabla ya siku hiyo ya kuniletea mimi Mungu wenu sadaka hiyo, hamruhusiwi kula mazao ya kwanza ya mavuno yenu, yawe mabichi, yamekaangwa au yemeokwa kuwa mikate. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu mahali popote mtakapoishi. “Mtahesabu majuma saba kamili tangu siku ile inayofuata Sabato ile ambapo mtaleta mganda wa sadaka ya kunitolea kwa ishara mimi Mwenyezi-Mungu. Mnamo siku ya hamsini, siku ya pili ya Sabato ya saba, mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya nafaka mpya. Kila jamaa italeta mikate miwili ya sadaka ya kutoa kwa ishara mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Kila mkate ni lazima uwe umetengenezwa kwa kilo mbili za unga laini uliotiwa chachu; na huo mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu ukiwa ni matoleo ya malimbuko yenu. Pamoja na hayo, mtatoa wanakondoo saba wa mwaka mmoja, fahali mchanga mmoja, na kondoo madume wawili. Wanyama hao watakuwa sadaka ya kuteketezwa pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji. Harufu ya sadaka hizi itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. Mtatoa beberu mmoja wa sadaka ya kuondoa dhambi na wanakondoo madume wawili wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka za amani. Kuhani atavipitisha mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu viwe sadaka ya kutoa kwa ishara pamoja na mkate wa mavuno ya kwanza na wale wanakondoo wawili. Vitu hivyo ni vitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu navyo vitakuwa kwa matumizi ya kuhani tu. Siku hiyohiyo mtatoa ilani ya mkutano mtakatifu; msifanye kazi. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu vyote, katika makazi yenu. “Unapovuna mavuno yako shambani, kamwe usivune kabisa hadi mpakani mwa shamba lako wala usirudi nyuma kukusanya masalio. Utawaachia hayo maskini na wageni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie watu wa Israeli hivi: Siku ya kwanza ya mwezi wa saba mtaadhimisha siku ya mapumziko rasmi, siku ya ukumbusho itakayotangazwa kwa mlio wa tarumbeta na kufanya mkutano mtakatifu. Msifanye kazi siku hiyo na ni lazima mnitolee mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa kwa moto.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni siku ya upatanisho. Siku hiyo ni siku ya kuwa na mkutano mtakatifu. Mtafunga na kutoa sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Msifanye kazi zenu zozote za kawaida siku hiyo. Siku hiyo ni siku ya upatanisho, siku ya kuwafanyieni upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mtu yeyote asiyefunga siku hiyo ni lazima atengwe mbali na watu wake. Mtu yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo nitamwangamiza miongoni mwa watu wake. Msifanye kazi: Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu, na katika makao yenu yote. Siku hiyo, itakuwa kwenu Sabato ya mapumziko rasmi na mtafunga. Siku ya Sabato ni siku ya kumi ya mwezi huo tangu jioni hadi jioni inayofuata.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Tangu siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba mtamfanyia Mwenyezi-Mungu sikukuu ya vibanda kwa muda wa siku saba. Hiyo ni sikukuu ya Mwenyezi-Mungu. Siku ya kwanza ya siku hizo saba, mtakuwa na mkutano mtakatifu na msifanye kazi. Kwa muda wa siku saba mtatoa sadaka anazopewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Siku ya nane mtakuwa na mkutano mkubwa na kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa. Mkutano huo ni mtakatifu. Siku hiyo msifanye kazi. “Hizo ndizo sikukuu za Mwenyezi-Mungu zilizopangwa ambazo mtatoa ilani kuwe na mkutano mtakatifu wa kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka zitolewazo kwa moto, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji, kila moja katika siku yake maalumu. Sadaka hizo ni pamoja na zile mnazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu siku ya Sabato kama vile pia sadaka zenu za kawaida, sadaka za kutimiza nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari mnazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu. “Baada ya kuvuna mashamba yenu mtafanya sikukuu kwa muda wa siku saba, tangu siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba. Siku ya kwanza itakuwa siku ya mapumziko na hata siku ya nane. Katika siku ya kwanza mtachukua matunda ya miti yenu mizuri, matawi ya mitende, matawi yenye majani mengi na matawi ya miti iotayo kandokando ya mto, nanyi mtafanya sherehe mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kwa siku saba. Kila mwaka ni lazima kuadhimisha sikukuu hii kwa muda wa siku saba kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu. Mtaifanya katika mwezi wa saba. Kwa muda wa siku saba mtaishi katika vibanda. Wakazi wote wa Israeli wataishi katika vibanda wakati huo. Jambo hilo litavijulisha vizazi vyenu kuwa nilipowatoa babu zenu nchini Misri, niliwafanya waishi katika vibanda. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Mose akawatangazia Waisraeli sikukuu za Mwenyezi-Mungu zilizopangwa. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waamuru watu wa Israeli wakuletee mafuta safi kwa ajili ya taa ili taa hiyo iendelee kuwaka daima. Aroni ataiweka taa hiyo ndani ya hema la mkutano, nje ya pazia la sanduku la maamuzi ili ipate kuwaka mbele yangu tangu usiku mpaka asubuhi. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu. Ataziweka hizo taa katika kinara cha taa cha dhahabu safi ziwake daima mbele ya Mwenyezi-Mungu. “Chukua unga laini, kilo kumi na mbili na kuoka mikate kumi na miwili. Mikate hiyo itapangwa safu mbili juu ya meza ya dhahabu safi, kila safu mikate sita. Kila safu utaitia ubani safi ili iambatane na mikate hiyo, na kuwa sehemu ya sadaka ya kuteketezwa ya ukumbusho kwa Mwenyezi-Mungu. Kila siku ya Sabato Aroni ataipanga sawasawa katika safu mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu kwa niaba ya watu wa Israeli kama agano la milele. Aroni na wazawa wake peke yao ndio wanaoruhusiwa kula mikate hiyo kwani ni mitakatifu kabisa kwa sababu ni sehemu ya sadaka ninazotolewa mimi Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hiyo ni haki yao milele.” Siku moja kukatokea mzozo huko kambini kati ya Mwisraeli mmoja na kijana mmoja wa mama Mwisraeli aitwaye Shelomithi lakini baba Mmisri. Siku moja yule kijana ambaye mama yake aliitwa Shelomithi binti Dibri wa kabila la Dani, alilikufuru na kulilaani jina la Mungu. Basi watu walimpeleka kijana kwa Mose, wakamtia ndani mpaka hapo watakapofunuliwa matakwa ya Mwenyezi-Mungu. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mtoe kijana aliyekufuru nje ya kambi, na wale wote waliomsikia akikufuru waweke mikono yao juu ya kichwa chake, na jumuiya yote imuue kwa kumpiga mawe. Nawe uwaambie Waisraeli kwamba mtu yeyote atakayemlaani Mungu wake ni lazima awajibike kwa dhambi yake. Mtu yeyote awe ni mwenyeji au mgeni anayemkufuru Mwenyezi-Mungu, jumuiya nzima itamuua kwa kumpiga mawe. Mtu yeyote anayeua mtu mwingine ni lazima naye auawe. Mtu yeyote anayeua mnyama ni lazima atoe fidia: Uhai kwa uhai. Mtu yeyote anayemwumiza jirani, ni lazima naye aumizwe kulingana na kiasi alichomwumiza jirani yake, amemvunja mfupa naye atavunjwa mfupa, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kila mtu anayemwumiza mwenzake ni lazima naye aumizwe kulingana na tendo lake. Anayemuua mnyama ni lazima atoe fidia; lakini mtu yeyote akimuua mtu mwingine ni lazima naye auawe. Sheria hii yamhusu mgeni na mwenyeji. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Basi, Mose akawaambia Waisraeli hayo yote. Wakampeleka yule mtu aliyemlaani Mwenyezi-Mungu nje ya kambi, wakamuua kwa kumpiga mawe. Ndivyo Waisraeli walivyofanya kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose huko mlimani Sinai, “Waambie Waisraeli hivi: Mtakapofika katika nchi ninayowapeni mimi Mwenyezi-Mungu kila mwaka wa saba nchi itapumzishwa isilimwe kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu. Kwa muda wa miaka sita mtailima nchi, mtapanda, mtapogoa mizabibu yenu na kuvuna mazao yenu. Lakini mwaka wa saba utakuwa ni sabato ya mapumziko rasmi; ni sabato ya Mwenyezi-Mungu. Msipande chochote wala kuipogoa mizabibu yenu. Chochote kinachoota peke yake msikivune wala kuchuma zabibu kutoka miti isiyopogolewa. Huo utakuwa mwaka wa kuipumzisha ardhi rasmi. Hata hivyo mwaka huo wa pumziko rasmi kwa nchi utawapa chakula nyinyi wenyewe, watumwa wenu wa kiume na wa kike, watu mliowaajiri na wageni wanaokaa miongoni mwenu. Nchi itailisha mifugo yenu na wanyama wa porini wanaokaa miongoni mwenu. “Mtahesabu miaka saba mara saba na jumla yake ni miaka arubaini na tisa. Kisha, katika siku ya kumi ya mwezi wa saba ambayo ni siku ya kufanyiwa upatanisho mtamtuma mtu kupiga tarumbeta katika nchi yote. Mwaka wa hamsini mtauheshimu kwa kutangaza uhuru kwa watumwa wote nchini. Mwaka huo utakuwa ni sikukuu ya ukumbusho wa miaka hamsini. Kila mmoja wenu atairudia mali yake na jamaa yake. Kwa kuwa mwaka huo, ni wa sikukuu ya ukumbusho wa miaka hamsini, msipande mbegu au kuvuna chochote kiotacho chenyewe wala kuchuma zabibu kutoka miti msiyoipogoa. Mwaka huo ni wa sikukuu kwenu; utakuwa mwaka mtakatifu. Hivyo mtakula yale yanayoota yenyewe mashambani. “Katika mwaka huo chochote ambacho kiliuzwa ni lazima kirudishwe kwa mwenyewe. Unaponunua au kuuza ardhi kwa jirani usimpunje. Bei ya ardhi ni lazima ilingane na miaka kabla ya kurudishwa kwa mwenyewe. Kama miaka inayohusika ni mingi utaongeza bei na kama miaka hiyo ni michache utapunguza bei, kwani bei yake itapimwa kulingana na mazao anayokuuzia. Msipunjane, bali, mtamcha Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Kwa hiyo, mtafuata masharti yangu na kutekeleza maagizo yangu, ili mpate kuendelea kuishi kwa usalama katika nchi. Nchi itatoa mazao yake nanyi mtakula na kushiba na kuishi humo kwa usalama. Lakini labda mtafikiri, ‘Tutakula nini katika mwaka wa saba iwapo haturuhusiwi kupanda wala kuvuna mazao yetu?’ Haya! Mimi nitaibariki nchi katika mwaka wa sita nayo itawapeni mazao ya kuwatosha kwa miaka mitatu. Mtakapopanda katika mwaka wa nane mtakuwa mnakula mazao ya zamani na mtaendelea kula tu hata mwaka wa tisa mtakapoanza tena kuvuna. “Kamwe ardhi isiuzwe kabisa, kwani hiyo ni mali yangu na nyinyi ni wageni na wasafiri nchini mwangu. Ndiyo maana katika nchi yote mtakuwa na utaratibu wa kuikomboa ardhi. “Kama ndugu yako anakuwa maskini, akauza ardhi yake, basi, ndugu yake wa karibu mwenye jukumu la kuikomboa, ataikomboa. Ikiwa mtu huyo hana ndugu mwenye jukumu la kuikomboa, lakini baadaye akawa tajiri na kupata uwezo wa kuikomboa ardhi yake, basi, atahesabu miaka inayohusika tangu alipoiuza na kulipa gharama zake; na yule mtu aliyeinunua ni lazima amrudishie. Lakini ikiwa hana uwezo wa kuikomboa, basi, itabaki mikononi mwa yule aliyeinunua mpaka mwaka wa sikukuu ya ukumbusho wa miaka hamsini. Katika mwaka huo, ni lazima mali hiyo iachiliwe na kurudishiwa yule mtu aliyeiuza. “Kama mtu akiuza nyumba yake ya kuishi iliyo ndani ya mji uliojengewa ukuta, ataweza kuikomboa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu alipoiuza. Kwa mwaka huo mzima atakuwa na haki ya kuikomboa. Kama nyumba iliyo katika mji uliojengewa ukuta haikukombolewa kwa muda wa mwaka mmoja, basi, itakuwa mali ya yule aliyeinunua milele katika vizazi vyao vyote; wala haitarudishwa katika mwaka wa sikukuu ya kukumbuka miaka hamsini. Lakini nyumba za vijiji ambavyo havikuzungushiwa ukuta zitakuwa chini ya sheria ileile ya ardhi; nyumba hizo zinaweza kukombolewa katika mwaka mmoja lakini ni lazima zirudishwe kwa wenyewe katika mwaka wa kukumbuka miaka hamsini. Hata hivyo, nyumba zilizomo katika miji wanayomiliki Walawi zinaweza kukombolewa wakati wowote. Ikiwa mmoja wa Walawi haitumii haki yake ya kukomboa, basi, nyumba iliyouzwa ni lazima irudishwe kwa mwenyewe katika mwaka wa kukumbuka miaka hamsini, kwani nyumba zilizomo katika miji wanayomiliki Walawi wamepewa kama sehemu yao kutoka kwa watu wa Israeli. Lakini mashamba wanayomiliki Walawi kwa pamoja, yasiuzwe, kwani huo ni urithi wao wa kudumu.” “Kama ndugu yako amekuwa maskini hata asiweze kujitunza mwenyewe akiwa pamoja nawe, ni lazima umtunze aendelee kuishi nawe; mtendee kama mgeni au msafiri aliye kwako. Usimtake akulipe riba ya namna yoyote ile. Ila mche Mungu, naye ndugu yako apate kuishi pamoja nawe. Usimkopeshe fedha kwa riba au kumpa chakula ili akulipe faida. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa nchini Misri ili kukupa nchi ya Kanaani, na ili nami niwe Mungu wako. “Kama ndugu yako anayeishi karibu nawe amekuwa maskini, akijiuza kwako, usimfanye akutumikie kama mtumwa. Atakaa nawe kama mtumishi aliyeajiriwa au kama msafiri. Atakutumikia hadi mwaka wa kuadhimisha miaka hamsini. Mwaka huo ni lazima umpe uhuru wake arudi kwa jamaa yake na urithi wa wazee wake; mwachie pamoja na jamaa yake. Kwa kuwa Waisraeli ni watumishi wangu ambao niliwatoa nchini Misri, basi, wasiuzwe kama watumwa. Usimtawale ndugu yako kwa ukatili, ila utamcha Mungu wako. Kuhusu watumwa, wa kike na wa kiume, unaweza kuwanunua kutoka kwa watu wa mataifa mengine ya jirani. Unaweza pia kununua watumwa kutoka kwa wageni wanaokaa pamoja nawe na jamaa zao waliozaliwa nchini mwenu; nao watakuwa mali yako. Hao watumwa unaweza kuwakabidhi kwa watoto wako wawe mali yao milele. Hao unaweza kuwafanya watumwa wako, lakini kuhusu ndugu yako Mwisraeli, usimtawale kwa ukatili. “Kama mgeni au msafiri anayekaa miongoni mwenu amekuwa tajiri na ndugu yako akawa maskini na kujiuza kwa huyo mgeni au huyo msafiri au kwa mmoja wa jamaa zao, anaweza kukombolewa baada ya kujiuza; mmojawapo wa ndugu zake anaweza kumkomboa. Mjomba wake anaweza pia kumkomboa, au binamu yake au ndugu wa karibu katika ukoo wake; anaweza pia kujikomboa yeye mwenyewe kama akiwa tajiri. Yeye akishirikiana na yule aliyemnunua, atahesabu idadi ya miaka tangu alipojiuza mpaka mwaka wa kuadhimisha kukumbuka miaka hamsini. Gharama ya kuachiliwa huru kwake italingana na miaka aliyomtumikia. Muda ambao amekuwa mtumwa wa bwana wake utapimwa kama muda wa mtumishi wa kuajiriwa. Kama idadi ya miaka mpaka mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini ni kubwa zaidi, basi atarudisha kiasi kikubwa cha bei aliyolipiwa. Kama miaka michache imepungua kabla ya kufikia sikukuu ya ukumbusho wa miaka hamsini, atahesabu kiasi cha bei iliyobaki kulingana na miaka hiyo na kumlipa hiyo fidia. Muda wote atakaokuwa kwa bwana wake ni lazima atendewe kama mtumishi aliyeajiriwa kila mwaka. Huyo aliyemnunua asimtendee kwa ukatili. Lakini ikiwa mtu huyo na jamaa yake hakukombolewa kwa njia hizo, basi apewe uhuru wake katika mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini. Waisraeli ni watumishi wangu, kwani niliwatoa katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Msijitengenezee sanamu za miungu ya uongo, msishike sanamu zao za kuchonga wala nguzo wala sanamu za mawe yaliyochongwa nchini mwenu na kuvisujudu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Shikeni sabato zangu na kuheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Kama mkifuata masharti yangu na kuzishika amri zangu, nitawanyeshea mvua wakati ufaao, nchi ipate kuzaa mavuno kwa wingi, nayo miti ya mashambani matunda yake. Kupura nafaka kutaendelea mpaka wakati wa kuvuna zabibu, na uvunaji zabibu mpaka wakati wa kupanda mbegu. Mtakuwa na chakula tele na kuishi kwa usalama nchini mwenu. Nitawapeni amani nchini hata muweze kulala bila ya kuogopeshwa na chochote. Nitawaondoa wanyama wakali katika nchi na nchi yenu haitakumbwa na vita. Mtawafukuza adui zenu na kuwaua kwa upanga. Watano wenu watawafukuza adui 100 na 100 wenu watawafukuza adui 10,000. Adui zenu wataangamia mbele yenu kwa upanga. Nitawafadhili na kuwajalia mpate watoto wengi na kuongezeka; nami nitaliimarisha agano langu nanyi. Wakati wa mavuno mtakuwa bado mnakula mazao ya zamani; tena itawalazimu kuondoa yaliyobaki kupata nafasi ya kuhifadhi mavuno mapya. Nitaweka maskani yangu miongoni mwenu, wala sitawaacheni. Nitatembea kati yenu na kuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa nchini Misri ili msiwe watumwa wa Wamisri. Mimi nimevunja nira mliyofungiwa shingoni mwenu na kuwafanya mtembee wima. “Lakini kama hamtanisikiliza wala kufuata amri zangu, kama mkidharau masharti yangu na kuchukia kwa roho maagizo yangu mkaacha kuzitii amri zangu zote na kuvunja agano langu, basi, mimi nitafanya hivi: Nitawapiga kwa kuwaletea hofu kuu ya ghafla, kifua kikuu na homa itakayowapofusha macho na kuwadhoofisha. Mtapanda mbegu zenu bila mafanikio kwani adui zenu ndio watakaokula. Mimi nitawakabili, nanyi mtapigwa na adui zenu; mtatawaliwa na wale wanaowachukia. Mtatishwa na kukimbia hata kama hakuna mtu yeyote anayewafukuza. Na Kama hata baada ya kuadhibiwa hivyo, hamtanisikiliza, basi, nitawaadhibu mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu. Kiburi chenu nitakivunjilia mbali kwa kuzifanya mbingu huko juu kuwa ngumu kama chuma, na nchi yenu bila mvua iwe ngumu kama shaba. Mtatumia nguvu zenu bure maana mashamba yenu hayatatoa mavuno na nchi yenu haitazaa matunda. “Kama mkiendelea kunipinga na kukataa kunisikiliza, nitazidisha tena adhabu yenu mara saba kadiri ya wingi wa dhambi zenu. Nitawapeleka wanyama wakali kati yenu ambao watawanyakulieni watoto wenu na kula mifugo yenu; na kukata idadi yenu hata njia zenu zigeuke kama jangwa. “Kama hata baada ya adhabu hiyo bado hamnigeukii mimi, ila mnazidi kupingana nami, basi, nami nitapingana nanyi na kuwaadhibu mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu. Nitawaleteeni upanga ambao utalipiza kisasi juu ya agano mlilovunja. Nyinyi mtakimbilia katika miji yenu, lakini nitawapelekea maradhi mabaya na kuwatia mikononi mwa adui zenu. Chakula chenu nitakipunguza hata wanawake kumi watumie jiko moja tu kuoka mikate. Watawagawia kwa kipimo. Na hata baada ya kula bado mtakuwa na njaa tu. “Na kama hata baada ya hayo yote bado hamtanisikiliza mkaendelea kunipinga, basi nami nitapingana nanyi kwa hasira kali, na kuwaadhibu mimi mwenyewe mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu. Ndipo mtakula watoto wenu, wa kiume na kike. Nitapaharibu mahali penu pa ibada milimani, nitazibomoa madhabahu zenu za kufukizia ubani, na kuzitupa maiti zenu juu ya sanamu za miungu yenu. Roho yangu itawachukia kabisa. Miji yenu nitaiteketeza mahali penu patakatifu nitapafanya jangwa na harufu zenu nzuri za sadaka kamwe sitazikubali. Nitaiteketeza nchi yenu hivyo kwamba hata adui wanaohamia humo watashangaa. Nitawatawanya nyinyi miongoni mwa watu wa mataifa na kuchomoa upanga dhidi yenu. Nchi yenu itakuwa ni ukiwa na miji yenu uharibifu. “Nyinyi mtakapokuwa mikononi mwa adui zenu, hapo ndipo nchi itakapozifurahia sabato zake wakati itakapokuwa hali ya ukiwa. Nchi itapumzika na kufurahia sabato zake. Kadiri itakapokuwa hali ya ukiwa itapata kiasi ambacho haikupata katika sabato zenu mlipokuwa mkiishi humo. Na kwa baadhi yenu watakaosalimika nitawaletea woga mioyoni mwao, katika nchi ya adui zao hata jani linalopeperushwa litawakimbiza. Watakimbia kama mtu anayekimbia vita. Watakimbia na kuanguka hata kama hamna mtu anayewafukuza. Wataangukiana ovyo kama mtu anayekimbia vita hata kama hamna anayewafukuza. Hamtakuwa na nguvu yoyote kuwakabili adui zenu. Mtaangamia kati ya mataifa na nchi za adui zenu zitawameza. Kama baadhi yenu wakisalimika katika nchi za adui zenu watadhoofika kwa sababu ya uovu wao; na kwa sababu ya uovu wa wazee wao. “Lakini kama wakitubu uovu wao na uovu wa wazee wao juu ya uasi waliotenda dhidi yangu na pia juu ya kupingana kwao nami, wakatambua kwa nini nilipingana nao na kuwapeleka katika nchi ya adui zao; kama kweli moyo wao mkaidi ukinyenyekea na kutubu uovu wao, basi, hapo nami nitalikumbuka agano langu na Abrahamu, Isaka na Yakobo; na kuikumbuka ile nchi niliyowaahidia. “Wakati watakapokuwa nje ya nchi yao, nchi hiyo itafurahia sabato zake hapo itakapokuwa hali ya ukiwa. Wakati huo wao watatubu uovu wao wa kupuuza maagizo yangu na kuyachukia maagizo yangu. Lakini, kwa hayo yote, wawapo katika nchi ya adui zao; mimi sitawatupa wala kuwachukia hata kuwaangamiza kabisa na kulivunjilia mbali agano langu. La! Kwa ajili yao nitalikumbuka agano nililofanya na wazee wao ambao niliwatoa katika nchi ya Misri, mataifa yakishuhudia, ili mimi niwe Mungu wao. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Hayo ndiyo masharti, maagizo na sheria ambazo Mwenyezi-Mungu aliwapa watu wa Israeli kule mlimani Sinai kwa njia ya Mose. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Mtu akiweka nadhiri ya kumtolea Mwenyezi-Mungu binadamu, mtu huyo anaweza kuondoa nadhiri yake kwa kulipa kiasi cha fedha kinachokadiriwa kama ifuatavyo: Mwanamume wa miaka ishirini hadi miaka sitini atakombolewa kwa fedha shekeli 50 kulingana na kipimo cha mahali patakatifu. Kama ni mwanamke, atakombolewa kwa fedha shekeli 30. Kama mtu huyo ni wa miaka kati ya mitano na 20 atakombolewa kwa fedha shekeli 20 kama ni mvulana na shekeli 10 za fedha kama ni msichana. Ikiwa ni mtoto wa umri wa kati ya mwezi mmoja na miaka mitano atakombolewa kwa shekeli 5 za fedha kama ni mvulana na shekeli 3 za fedha kama ni msichana. Ikiwa mtu huyo umri wake ni zaidi ya miaka sitini, thamani yake itakuwa ni shekeli 15 za fedha kama ni mwanamume na shekeli 10 za fedha kama ni mwanamke. Lakini ikiwa mtu huyo ni maskini na hawezi kulipa gharama yake, basi, mtu huyo atapelekwa kwa kuhani. Kuhani atampima thamani yake kulingana na uwezo wa huyo aliyeweka nadhiri. “Ikiwa nadhiri yenyewe inahusu mnyama wa namna ambayo watu humtolea Mwenyezi-Mungu sadaka, basi mnyama huyo huwa kitu kitakatifu. Hairuhusiwi kumbadilisha mnyama huyo kwa mwingine awaye yeyote, mzuri kwa mbaya au mbaya kwa mzuri. Kama akimbadilisha kwa mnyama mwingine, wote wawili watakuwa watakatifu. “Kama nadhiri hiyo yahusu mnyama najisi, wa aina ambayo si halali kumtolea Mwenyezi-Mungu, basi, mtu aliyemtoa, atamleta kwa kuhani, naye kuhani ataamua thamani yake kulingana na uzuri au ubaya wake. Jinsi atakavyoamua kuhani, ndivyo itakavyokuwa. Lakini ikiwa mwenyewe anataka kumkomboa, basi, ataongeza asilimia ishirini ya thamani ya mnyama huyo. “Mtu akiiweka wakfu nyumba yake kuwa takatifu kwa Mwenyezi-Mungu, kuhani ataamua thamani yake kulingana na uzuri au ubaya wake. Jinsi atakavyoamua, ndivyo itakavyokuwa. Kama huyo mtu aliyeiweka wakfu akitaka kuikomboa hiyo nyumba, basi, ataongeza asilimia ishirini ya thamani yake, nayo itakuwa mali yake. “Mtu akiiweka ardhi yake, ambayo ni urithi wake, wakfu kwa Mwenyezi-Mungu basi, thamani yake itapimwa kulingana na mbegu zinazotumika kulipanda shamba hilo; kwa kila kilo ishirini za shayiri thamani yake itakuwa shekeli hamsini za fedha. Kama akiliweka wakfu shamba lake katika mwaka wa kuadhimisha miaka hamsini, thamani yake ni lazima ilingane na vipimo vyenu. Lakini kama akiliweka wakfu baada ya mwaka huo, basi, kuhani ataamua thamani yake kulingana na miaka iliyobaki kufikia mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini na thamani yake ipunguzwe. Kama mwenyewe akitaka kulikomboa, basi, ni lazima aongeze asilimia ishirini ya thamani ya shamba hilo, na kisha litakuwa mali yake. Lakini kama hataki kulikomboa au amemwuzia mtu mwingine, basi, shamba hilo lisikombolewe tena. Katika mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini shamba hilo litaachiliwa na kuwa lake Mwenyezi-Mungu milele. Kuhani ndiye atakayelimiliki. “Kama mtu akiweka wakfu shamba alilonunua, yaani sio lake kwa urithi, kuhani ataamua thamani ya shamba hilo kwa kulingana na miaka iliyobaki kufikia mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini na mtu huyo atalazimika kulipa thamani yake kama ni kitu kitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu. Lakini katika mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini, shamba hilo ni lazima arudishiwe yule mtu aliyeliuza. Kila thamani itapimwa kwa kipimo cha uzito cha shekeli kulingana na kipimo cha mahali patakatifu: Uzito wa gera 20 ni sawa na uzito wa shekeli moja. “Hairuhusiwi kumweka wakfu mzaliwa wa kwanza wa wanyama; kisheria huyo ni wake Mwenyezi-Mungu; awe ni ng'ombe au kondoo. Kama anayehusika ni mnyama najisi, mwenyewe atamnunua kwa kulingana na mnavyompima na ataongeza asilimia ishirini ya thamani ya mnyama huyo. Kama hakombolewi, basi, atauzwa kulingana na vipimo vyenu. “Lakini kitu chochote kilichowekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, kiwe ni mtu au mnyama au kitu kilichopatikana kwa urithi, hakitauzwa wala kukombolewa. Chochote kilichowekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu ni kitakatifu kabisa. Mtu yeyote aliyewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu ili aangamizwe, asikombolewe; sharti auawe. “Zaka za mazao iwe ni nafaka au matunda ya miti, yote ni mali ya Mwenyezi-Mungu; ni takatifu kwa Mwenyezi-Mungu. Kama mtu akitaka kuikomboa zaka yake, atalipa thamani yake na kuongeza asilimia ishirini ya thamani ya zaka hiyo. Kuhusu mifugo, inapohesabiwa, kila mnyama wa kumi ni mtakatifu kwa Mwenyezi-Mungu. Mtu yeyote hana ruhusa kuuliza kama mnyama huyo ni mzuri au mbaya wala mnyama huyo kamwe hatabadilishwa kwa mwingine. Kama akibadilishwa kwa mwingine, wanyama wote wawili watakuwa watakatifu; hawatakombolewa.” Hizo ndizo amri ambazo Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose ili awaambie Waisraeli, mlimani Sinai. Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa pili, mwaka wa pili baada ya wana wa Israeli kutoka Misri, Mwenyezi-Mungu aliongea na Mose ndani ya hema la mkutano jangwani Sinai, akamwambia hivi: “Wewe na Aroni fanyeni sensa ya jumuiya yote ya Waisraeli, familia mojamoja kwa kufuata koo zao na idadi ya majina yao kila mwanamume mmojammoja; wale wote katika Israeli wanaoweza kwenda vitani, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, mtawaweka katika orodha ya vikosi vikosi. Tena mwanamume mmoja wa kila kabila atakuwa pamoja nanyi, kila mmoja aliye kiongozi wa jamaa za kabila lake. Haya ndiyo majina ya watu watakaokusaidia: Kabila la Reubeni: Elisuri, mwana wa Shedeuri; Kabila la Simeoni: Shelumieli mwana wa Suri-shadai; Kabila la Yuda: Nashoni mwana wa Aminadabu; Kabila la Isakari: Nethaneli mwana wa Suari; Kabila la Zebuluni: Eliabu mwana wa Heloni; Kabila la Efraimu: Elishama mwana wa Amihudi; Kabila la Manase: Gamalieli mwana wa Pedasuri; Kabila la Benyamini: Abidani mwana wa Gideoni; Kabila la Dani: Ahiezeri mwana wa Amishadai; Kabila la Asheri: Pagieli mwana wa Okrani; Kabila la Gadi: Eliasafu mwana wa Deueli; Kabila la Naftali: Ahira mwana wa Enani.” Hawa ndio viongozi waliochaguliwa miongoni mwa jumuiya yote ya watu wa Israeli, kama viongozi wakuu wa makabila yao na viongozi wa koo za Israeli. Basi, Mose na Aroni wakawachukua watu hawa waliotajwa, na mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa pili, wakaikusanya jumuiya yote ya watu waliokuwa wamehesabiwa kila mmoja kulingana na familia yake na ukoo wake. Kufuatana na majina ya watu waliokuwa na umri wa miaka ishirini na zaidi, mmojammoja, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Mose akawahesabu watu hawa kule jangwani Sinai. Watu waliotoka katika kabila la Reubeni aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Israeli, kwa kufuata vizazi vyao, kulingana na familia zao na jamaa zao, kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, kila mwanamume aliyekuwa na umri wa miaka ishirini na zaidi, aliyefaa kuingia jeshini, walikuwa watu 46,500. Kutoka kabila la Simeoni kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 59,300. Kutoka kabila la Gadi kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 45,650. Kutoka kabila la Yuda kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 74,600. Kutoka kabila la Isakari kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 54,400. Kutoka kabila la Zebuluni kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 57,400. Kutoka kabila la Efraimu, mwanawe Yosefu, kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 40,500. Kutoka kabila la Manase, mwanawe Yosefu, kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 32,200. Kutoka kabila la Benyamini, kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 35,400. Kutoka kabila la Dani kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 62,700. Kutoka kabila la Asheri, kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 41,500. Kutoka kabila la Naftali, kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina ya mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, walikuwa watu 53,400. Hawa ndio watu waliokuwa wamehesabiwa ambao Mose na Aroni waliwahesabu wakisaidiwa na wale viongozi kumi na wawili wa Israeli, kila kiongozi akiwakilisha ukoo wake. Hivyo jumla ya wanaume wote wa Israeli wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini nchini Israeli ilikuwa watu 603,550. Lakini Walawi hawakuhesabiwa pamoja na yale makabila mengine, kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Usihesabu kabila la Lawi wala usiwafanyie sensa kati ya watu wa Israeli; bali utawateua wawe waangalizi wa hema la ushuhuda, vyombo vyake vyote na kila kitu kilichomo ndani yake; watakuwa wakilibeba pamoja na vyombo vyake vyote. Watahudumu humo ndani na kupiga kambi yao kwa kulizunguka. Tena wakati wa hema kungolewa Walawi ndio watakaolingoa na wakati wa hema kusimikwa Walawi ndio watakaolisimamisha. Waisraeli wengine wote watapiga kambi zao makundimakundi, kila mtu katika kundi lake na chini ya bendera yake. Lakini Walawi watapiga kambi zao kulizunguka hema la maamuzi, wakililinda ili mtu yeyote asije akalikaribia na kusababisha ghadhabu yangu kuwaka dhidi ya jumuiya ya watu wa Israeli; basi Walawi watalitunza hema la maamuzi.” Kwa hiyo Waisraeli wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Mwenyezi-Mungu aliwapa Mose na Aroni, maagizo yafuatayo: “Waisraeli watapiga kambi zao, kila mmoja akikaa mahali penye bendera yake, penye alama za ukoo wake. Watapiga kambi zao kulizunguka hema la mkutano. “Wale watakaopiga kambi upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua watakuwa kikundi cha watu walio chini ya bendera ya Yuda na kiongozi wao atakuwa Nashoni mwana wa Aminadabu, kikosi chake kulingana na hesabu ni wanaume 74600. Wale watakaofuata kupiga kambi baada ya watu wa Yuda watakuwa kabila la Isakari, kiongozi wao akiwa Nethaneli mwana wa Suari, kikosi chake kulingana na hesabu ni wanaume 54,400. Kisha kabila la Zebuluni, kiongozi wao akiwa Eliabu mwana wa Heloni, kikosi chake kulingana na hesabu ni wanaume 57,400. Jumla yote ya watu watakaokuwa katika kambi ya Yuda kulingana na makundi yao ni watu 186,400. Hao ndio watakaotangulia kusafiri. “Kwa upande wa kusini, wale walio chini ya bendera ya kundi la Reubeni kulingana na makundi yao, kiongozi wao akiwa Elisuri mwana wa Shedeuri, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 46,500. Kisha wale watakaopiga kambi kando ya watu wa Reubeni watakuwa ni watu wa kabila la Simeoni, kiongozi wao akiwa Shelumieli mwana wa Suri-shadai, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 59,300. Hatimaye kabila la Gadi, kiongozi wao akiwa Eliasafu mwana wa Reueli, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 45,650. Jumla ya wanaume watakaokuwa katika kambi ya Reubeni kulingana na makundi yao ni watu 151,450. Hawa ndio watakaokuwa katika msafara wa pili. “Halafu, kambi ya kabila la Walawi, ikiwa katikati ya kambi zote, na wakiwa wamebeba hilo hema la mkutano, wataondoka; kila kundi litasafiri kwa kufuata nafasi yake chini ya bendera yao. “Kwa upande wa magharibi, wale walio chini ya bendera ya kundi la Efraimu watapiga kambi kulingana na makundi yao, kiongozi wao akiwa Elishama mwana wa Amihudi, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 32,200. Mara tu baada ya Waefraimu litafuata kabila la Manase: Kiongozi wake akiwa Gamalieli, mwana wa Pedasuri, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa watu 32,000. Hatimaye kabila la Benyamini: Kiongozi wake ni Abidani, mwana wa Gideoni, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 35,400. Jumla ya watu watakaokuwa katika kambi ya Efraimu kulingana na makundi yao ni watu 108,100. Kundi hili la Efraimu litakuwa katika msafara wa tatu. “Kwa upande wa kaskazini, watapiga kambi katika makundi yao wale walio chini ya bendera ya Dani, kiongozi wao atakuwa Ahiezeri, mwana wa Amishadai, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 62,700. Kisha wale watakaopiga kambi baada yao watakuwa watu wa kabila la Asheri, kiongozi wao akiwa Pagieli mwana wa Okrani, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 41,500. “Hatimaye watu wa kabila la Naftali, kiongozi wake akiwa Ahira mwana wa Enani, kikosi chake kulingana na hesabu, kitakuwa na watu 53,400. Jumla ya watu watakaokuwa katika kambi ya Dani kulingana na makundi yao ni watu 157,600. Kundi hili la Dani litakuwa katika msafara wa mwisho, bendera baada ya bendera.” Hao ndio Waisraeli waliohesabiwa kulingana na koo zao, katika kambi na vikosi vyao; wote walikuwa 603,550. Lakini Walawi hawakuhesabiwa miongoni mwa watu wa Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Hivyo ndivyo, Waisraeli walivyofanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Walipiga kambi zao, kufuata bendera zao na walisafiri kila mmoja akiandamana na jamaa yake kwa kufuata ukoo wake. Wafuatao ndio wazawa wa Aroni na Mose wakati Mwenyezi-Mungu alipozungumza na Mose mlimani Sinai. Haya ndiyo majina ya wana wa Aroni: Nadabu, mzaliwa wake wa kwanza, Abihu, Eleazari na Ithamari. Hawa waliwekwa wakfu kwa kupakwa mafuta wawe makuhani. Lakini Nadabu na Abihu walikufa mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakati walipomtolea Mwenyezi-Mungu moto usio mtakatifu katika jangwa la Sinai. Wao hawakuwa na watoto kwa hiyo Eleazari na Ithamari wakawa wanahudumu kama makuhani wakati wa uhai wa Aroni baba yao. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Walete karibu watu wa kabila la Lawi, uwaweke mbele ya kuhani Aroni ili uwape jukumu la kumtumikia. Watafanya kazi kwa niaba yake na ya jumuiya yote kwenye hema la mkutano wanapohudumu mahali patakatifu, wataangalia na kutunza vyombo vyote vya hema la mkutano na kuwasaidia Waisraeli wanapotoa huduma zao kwenye mahali patakatifu. Walawi utampa Aroni na wazawa wake makuhani; hao wametolewa kati ya Waisraeli wawahudumie kabisa. Utawateua Aroni na wanawe ili waweze kutekeleza huduma zao za ukuhani; lakini kama mtu yeyote mwingine atakaribia, atauawa.” Mwenyezi-Mungu akaendelea kumwambia Mose, “Angalia, sasa nimewateua Walawi miongoni mwa Waisraeli wote, badala ya kila mzaliwa wa kwanza wa kiume kifunguamimba katika kila familia ya Israeli. Walawi ni wangu, kwani kila mzaliwa wa kwanza katika Israeli ni wangu. Wakati nilipowaua wazaliwa wa kwanza wote wa Wamisri nilijiwekea wakfu kila mzaliwa wa kwanza katika Israeli; kila mzaliwa wa kwanza wa binadamu hata wa mnyama; wao watakuwa wangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Baadaye Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose katika jangwa la Sinai, “Wahesabu wana wa Lawi wote kulingana na koo zao na familia zao, kila mwanamume kuanzia watoto wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi.” Basi, Mose akawahesabu kufuatana na neno la Mwenyezi-Mungu, kama alivyomwamuru. Wafuatao ndio waliokuwa wana wa Lawi: Gershoni, Kohathi na Merari. Na haya ndiyo majina ya wana wa Gershoni kwa kufuata familia zao: Libni na Shimei. Wana wa Kohathi kwa kufuata familia zao: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli. Wana wa Merari kwa kufuata familia zao: Mahli na Mushi. Hizi zilikuwa jamaa za Walawi kulingana na koo zao. Familia za Walibni na Washimei zilitokana na Gershoni; hizi ndizo zilizokuwa jamaa za Wagershoni. Idadi yao kwa kadiri ya hesabu ya wanaume wote kuanzia waliokuwa na mwezi mmoja na zaidi ni 7,500. Familia za Wagershoni, iliwapasa kupiga kambi yao upande wa magharibi, nyuma ya hema takatifu naye Eliasafu mwana wa Laeli akiwa mkuu wa ukoo wa Wagershoni. Kazi ya wana wa Gershoni ilikuwa kulitunza hema takatifu, hema pamoja na kifuniko chake, pazia la mlango wa hema la mkutano, mapazia ya ua ulioko kati ya hema takatifu na madhabahu, na pazia la mlango wa ua, na kamba zake. Huduma zote zilizohusu vitu hivi zilikuwa zao. Familia za Waamrami, Waishari, Wahebroni na Wauzieli zilitokana na Kohathi; hizi ndizo zilizokuwa jamaa za Wakohathi. Kadiri ya hesabu ya wanaume wote kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi ilikuwa 8,600, waliohusika na huduma za mahali patakatifu. Familia za wana wa Kohathi zilitakiwa kupiga kambi yao upande wa kusini wa mahali patakatifu, naye Elisafani, akiwa mkuu wa ukoo huo wa familia za Wakohathi. Wajibu wao ulikuwa kulitunza sanduku la agano, meza, kinara cha taa, madhabahu, vyombo wanavyotumia makuhani mahali patakatifu na pazia; huduma zote zilizohusu vitu hivi zilikuwa zao. Naye Eleazari mwana wa kuhani Aroni aliwekwa kuwa mkuu wa wakuu wa Walawi, na msimamizi wa wahudumu wote wa mahali patakatifu. Familia za Wamahli na Wamushi zilitokana na Merari. Hizi ndizo familia za Merari. Idadi yao kadiri ya hesabu ya wanaume wote kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi ilikuwa watu 6,200. Mkuu wa ukoo wa familia za Merari alikuwa Surieli mwana wa Abihaili; hawa walitakiwa kupiga kambi yao upande wa kaskazini wa hema takatifu. Wao walipewa kazi ya kutunza mbao za hema takatifu, mataruma, nguzo, vitako na vifaa vyote vya kushikilia hema; huduma zote zilizohusu vitu hivi zilikuwa juu yao. Pia walihitajika kutunza nguzo za ua zilizouzunguka na vitako vyake, vigingi na kamba zake. Mose na Aroni na wana wao walitakiwa kupiga kambi yao mbele ya hema takatifu upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua. Wajibu wao ulikuwa kutoa huduma kwenye mahali patakatifu kwa lolote lililohitajika kufanyika kwa ajili ya Waisraeli. Mtu mwingine yeyote aliyesogea karibu ilibidi auawe. Idadi ya Walawi kulingana na familia zao, wanaume wote kuanzia watoto wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi ambao Mose na Aroni waliwahesabu kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, ilikuwa watu 22,000. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Wahesabu kwa majina wazaliwa wa kwanza wa kiume wote wa Waisraeli kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi. Nawe utatenga Walawi kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu; pia utatenga kwa ajili yangu mifugo yote ya Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo ya watu wa Israeli.” Basi, Mose akawahesabu wazaliwa wa kwanza wote wa watu wa Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru. Wazaliwa wote wa kwanza wa kiume kadiri ya hesabu ya majina, kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi, kufuata walivyohesabiwa, walikuwa 22,273. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Sasa, watenge Walawi wote kuwa wangu badala ya wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli. Kadhalika, watenge ng'ombe wa Walawi wote badala ya wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe wa Waisraeli. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. Kwa ajili ya fidia ya wazaliwa wa kwanza wa kiume wa watu wa Israeli 273, wanaozidi idadi ya wanaume Walawi, utapokea kwa kila mwanamume fedha shekeli tano, kulingana na kipimo cha mahali patakatifu, ambayo ni sawa na gera ishirini, na fedha hizo kwa ajili ya fidia ya hao waliozidi idadi yao utampa Aroni na wanawe.” Mose akatii, akachukua fedha hizo za fidia ya hao waliozidi idadi ya waliofidiwa na Walawi; alipokea kutoka wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli fedha kiasi cha shekeli 1,365, kulingana na kipimo cha mahali patakatifu, akawapa Aroni na wanawe fedha hizo za fidia sawa na neno la Mwenyezi-Mungu kama alivyomwamuru. Mwenyezi-Mungu akawaambia Mose na Aroni, “Wahesabu watu wa ukoo wa Kohathi, mmoja wa koo za Lawi, kufuatana na jamaa zao na koo zao; utawaorodhesha wanaume wote wenye umri kati ya miaka thelathini na hamsini wanaofaa kujiunga na huduma ya hema la mkutano. Hii ndio itakayokuwa huduma ya wana wa Kohathi, kuhusu vitu vitakatifu kabisa. “Wakati wa kuvunja kambi, Aroni na wanawe wataingia katika hema, na kulishusha pazia lililoko mbele ya sanduku la agano, kisha walifunike kwa pazia hilo. Juu yake wataweka kifuniko cha ngozi laini ya mbuzi, kisha watatandaza kitambaa cha rangi ya buluu safi. Halafu wataingiza mipiko ya kulichukulia sanduku hilo. “Juu ya meza ya kutolea mikate inayowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu watatandaza kitambaa cha buluu ambacho juu yake wataweka sahani, visahani vya ubani, bakuli na bilauri, kwa ajili ya kutolea tambiko za kinywaji. Daima kutakuwa na mkate juu ya meza. Kisha, watavifunika vyombo hivi vyote kwa kitambaa chekundu, na juu yake wataweka kifuniko cha ngozi laini ya mbuzi. Halafu wataingiza mipiko yake ya kulibeba. “Watachukua kitambaa cha buluu ambacho watafunikia kinara cha taa na taa zake, makasi zake, sinia zake na vyombo vyote vinavyotumiwa kukiwekea mafuta. Watakiweka pamoja na vyombo vyake vyote ndani ya ngozi laini ya mbuzi na kukiweka juu ya mipiko ya kuchukulia. “Halafu watatandaza kitambaa cha buluu juu ya madhabahu ya dhahabu na kuifunika kwa ngozi laini ya mbuzi juu yake. Halafu wataingiza mipiko yake ya kuichukulia. Watavichukua vyombo vyote vinavyotumika mahali patakatifu, watavifunga kwa kitambaa cha buluu na kuvifunika kwa ngozi laini ya mbuzi, kisha wataviweka juu ya mipiko yake ya kuchukulia. Watayaondoa majivu kutoka madhabahuni na juu yake watatandaza kitambaa cha zambarau. Juu yake wataviweka vyombo vyote vitumikavyo katika ibada kwenye madhabahu: Vyetezo, nyuma, miiko na mabakuli. Kisha, juu yake watatandaza kifuniko cha ngozi laini ya mbuzi na kuiingiza mipiko yake ya kulibebea. Baada ya Aroni na wanawe kupafunika mahali patakatifu pamoja na vyombo na vifaa vyake vyote, wakiwa tayari kuanza safari, watu wa ukoo wa Kohathi watakuja na kuvibeba. Lakini wao, hawaruhusiwi kabisa kuvigusa vyombo hivyo vitakatifu, wasije wakafa. Hiyo ndiyo kazi ya ukoo wa Kohathi kila wakati hema la mkutano linapohamishwa. Eleazari mwana wa kuhani Aroni itampasa kuyatunza mafuta ya taa, ubani wa kunukia, tambiko za nafaka za kila siku, mafuta ya kupaka ili kuweka wakfu na kila kitu kilichowekwa wakfu katika hema hilo.” Kisha Mwenyezi-Mungu akawaambia Mose na Aroni, “Msiache ukoo wa familia za Kohathi miongoni mwa Walawi uangamizwe. Basi, ili kuwaepusha wasije wakauawa kwa kuvikaribia vyombo hivyo vitakatifu sana utafanya hivi: Aroni na wanawe wataingia na kumpangia kila mmoja wao wajibu wake na kazi yake. Lakini wazawa wa Kohathi hawataingia kamwe kuvitazama vitu hivyo vitakatifu sana; wakifanya hivyo watakufa.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Wahesabu watu wa ukoo wa Gershoni, kufuatana na familia na koo zao; utawahesabu wanaume wote wenye umri kati ya miaka thelathini na hamsini wanaofaa kujiunga na huduma ya hema la mkutano. Wajibu wao utakuwa huu: Watabeba mapazia ya hema takatifu na hema la mkutano pamoja na kifuniko chake, kifuniko cha ngozi laini ya mbuzi kilicho juu yake, pazia la lango, mapazia na kamba za ua ulio kandokando ya hema na madhabahu, mapazia ya lango la kitalu, na vifaa vyote vinavyotumika pamoja na vitu hivi. Wao watashughulika na mambo yote yanayohusika na vitu hivi. Aroni na wanawe makuhani ndio watakaoamrisha huduma zote za Wagershoni kuhusu vitu watakavyobeba na kazi watakazofanya. Utawapangia vitu vyote vile ambavyo wanapaswa kubeba. Hii ndiyo huduma ya jamaa za Gershoni kwenye hema la mkutano; watafanya kazi chini ya uongozi wa Ithamari mwana wa kuhani Aroni. “Kadhalika, utawahesabu wana wa Merari, kufuatana na jamaa zao na koo zao. Utawahesabu wanaume wote wenye umri kati ya miaka thelathini na hamsini, wanaofaa kujiunga na huduma ya hema la mkutano. Wao, watakuwa na wajibu na kubeba mbao, mataruma, nguzo na misingi ya hema la mkutano. Kadhalika na nguzo za ua za kuzunguka pande zote, vikalio, vigingi na kamba pamoja na vifaa vyake vyote na vyombo vyake vingine vyote. Nawe utawapangia kufuata majina yao vitu watakavyopaswa kubeba. Hii ndiyo itakayokuwa kazi ya wana wa ukoo wa Merari katika huduma yao yote ndani ya hema la mkutano, chini ya uongozi wa Ithamari mwana wa kuhani Aroni.” Basi, Mose, Aroni na viongozi wa jumuiya yote wakafanya sensa ya watu wa ukoo wa Kohathi, kufuatana na familia zao, wakawaorodhesha watu wote wenye umri kati ya miaka thelathini na hamsini, kila aliyefaa kuingia katika huduma ya hema la mkutano. Idadi yao kufuatana na jamaa zao ilikuwa watu 2,750. Hii ndiyo idadi ya watu wa jamaa ya Kohathi, ambao walihudumu katika hema la mkutano, ambao Mose na Aroni waliwahesabu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Idadi ya watu wa ukoo wa Gershoni kufuatana na familia zao, wenye umri kati ya miaka thelathini na hamsini, waliofaa kuhudumu katika hema la mkutano, ilikuwa watu 2,630. Hii ndiyo iliyokuwa idadi ya watu wa familia za wana wa Gershoni wote waliohudumu katika hema la mkutano, ambao Mose na Aroni waliwahesabu kama Mwenyezi-Mungu alivyowaagiza. Idadi ya watu wa ukoo wa Merari kufuatana na jamaa zao na familia zao, wenye umri kati ya miaka thelathini na hamsini, waliofaa kuhudumu katika hema la mkutano, ilikuwa watu 3,200. Hii ndiyo idadi ya watu wa ukoo wa Merari ambao Mose na Aroni waliwahesabu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza Mose. Hivyo, Walawi wote walioandikishwa na Mose, Aroni na viongozi wa watu, kwa kufuata jamaa zao na koo zao, wenye umri kati ya miaka thelathini na hamsini, na ambao walifaa kwa huduma na uchukuzi katika hema la mkutano, jumla walikuwa watu 8,580. Kila mmoja alipewa kazi yake ya kufanya kuhusu kubeba hema la mkutano, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waamuru Waisraeli wamtoe nje ya kambi kila mtu mwenye ukoma, kila mtu anayetokwa usaha, na kila aliye najisi kwa kugusa maiti. Mtawatoa nje ya kambi watu wote hawa, wanaume kwa wanawake, ili wasije wakaitia najisi kambi yangu ninamokaa.” Waisraeli walifanya hivyo, wakawafukuza nje ya kambi. Kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose, ndivyo Waisraeli walivyofanya. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli kuwa: Mtu yeyote, mwanamume au mwanamke akitenda dhambi dhidi ya mtu, akakosa uaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, mtu huyo ana hatia; itambidi aungame dhambi yake aliyotenda. Lazima atoe fidia kamilifu kwa kosa lake, akiongeza asilimia ishirini ya fidia hiyo; atampa fidia hiyo yule aliyemkosea. Lakini ikiwa mtu huyo amefariki na hana jamaa wa karibu ambaye anaweza kupokea fidia hiyo, basi, fidia ya kosa itatolewa kwa Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya makuhani; malipo haya ni pamoja na kondoo dume wa upatanisho ambaye atatumiwa kumfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake. Michango yote na matoleo yote ambayo Waisraeli wataweka wakfu kwa Mungu na kumletea kuhani itakuwa yake huyo kuhani. Kila kitu kilichowekwa wakfu kwa Mungu na kupelekwa kwa kuhani kitakuwa chake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli: Kama mke wa mtu yeyote amepotoka akakosa uaminifu kwa mumewe, akalala na mtu mwingine bila ya mumewe au mtu mwingine yeyote kujua; amejitia najisi lakini hakuna mtu aliyeshuhudia kitendo chake kwa kuwa hakufumaniwa. Basi, mumewe akiingiwa na shaka na kuwa na wivu juu ya mkewe aliyejitia najisi; au kama amekuwa na wivu juu ya mke wake ingawa mkewe hakujitia najisi, basi wote wawili watakwenda kwa kuhani na kupeleka sadaka inayotakiwa, yaani sehemu ya kumi ya unga wa shayiri; lakini bila kuitia mafuta au ubani, kwa kuwa ni sadaka ya nafaka ya mume anayemshuku mkewe, sadaka inayotolewa kuhusu kosa ambalo linabainishwa. “Kuhani atampeleka huyo mwanamke karibu, na kumsimamisha mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kisha, atamimina maji matakatifu katika chombo cha udongo na kutwaa vumbi kutoka sakafuni mwa hema takatifu na kuitia katika maji hayo ili kuyafanya machungu. Kuhani atamweka mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumfunua nywele na kumpa sadaka hiyo ya nafaka itolewayo kwa sababu ya shuku ya mumewe. Kuhani mwenyewe atashikilia kile chombo chenye maji machungu yaletayo laana. Halafu kuhani atamwapisha mwanamke huyo akisema: ‘Ikiwa hukulala na mwanamume mwingine, ukajitia najisi hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, basi, hutapatwa na laana iletwayo na maji haya machungu. Lakini kama umepotoka hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, ukajitia najisi kwa kulala na mwanamume mwingine asiye mume wako, Mwenyezi-Mungu na akuadhibu hata uwe laana na apizo miongoni mwa watu wako, uwe tasa na tumbo lako livimbe. Maji haya yaletayo laana na yaingie tumboni mwako na kukufanya tasa na tumbo lako livimbe.’ Naye mwanamke ataitikia, ‘Amina, Amina.’ “Kisha kuhani ataandika laana hizi kitabuni na kuzioshea katika maji machungu; naye atamnywesha mwanamke hayo maji machungu yaletayo laana nayo yataingia ndani yake na kumletea maumivu makali; kisha kuhani atachukua ile sadaka ya nafaka ya wivu mikononi mwa mwanamke huyo na kuitikisa mbele ya Mwenyezi-Mungu, na kuipeleka madhabahuni. Halafu, atatwaa konzi moja ya sadaka hiyo ya nafaka kwa ukumbusho na kuiteketeza madhabahuni. Hatimaye atamnywesha mwanamke maji hayo. Akisha kunywa, kama amejitia najisi na hakuwa mwaminifu kwa mume wake, maji hayo yaletayo laana yatamletea maumivu makali sana; mwili wake utavimba na tumbo lake la uzazi litaharibika. Mwanamke huyo atakuwa laana miongoni mwa watu wake. Lakini kama mwanamke huyo hajajitia unajisi na hana hatia, basi hatadhurika na ataweza kupata watoto. “Basi, hii ndiyo sheria kuhusu kesi za wivu iwapo mwanamke, ingawa yu chini ya mamlaka ya mumewe, atapotoka na kujitia unajisi, au wakati mwanamume ashikwapo na wivu na kumshuku mkewe. Atamsimamisha mwanamke huyo mbele ya Mwenyezi-Mungu, na kuhani atatekeleza masharti yote ya sheria hii. Mumewe hatakuwa na hatia yoyote, lakini mwanamke atawajibika kwa uovu wake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Wape Waisraeli maagizo yafuatayo: Iwapo mwanamume au mwanamke ataweka nadhiri maalumu, nadhiri ya kujiweka wakfu, akajitenga kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu, basi, asinywe divai au kileo, asinywe siki ya divai au ya namna nyingine, asinywe maji ya zabibu wala kula zabibu zilizoiva au kavu. Muda wote atakaokuwa mnadhiri asile kitu chochote kinachotokana na mzabibu, tangu kokwa hata maganda yake. “Siku zote za nadhiri yake ya kujitenga, hatanyoa nywele zake; mpaka muda wa nadhiri yake ya kujiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu utakapomalizika, atakuwa mtakatifu, ataziacha nywele zake ziwe ndefu. Siku zote atakazokuwa amejiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, mtu huyo asikaribie maiti, hata kama ni ya baba, mama, ndugu au dada yake, asije akajitia unajisi kwa maana amejiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu kwa kiapo. Muda wote atakaokuwa mnadhiri atakuwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. “Endapo nywele za mnadhiri zitatiwa unajisi mtu afapo ghafla karibu naye, atakinyoa kichwa chake wakati wa siku ya kutakaswa kwake; atakinyoa katika siku ya saba. Katika siku ya nane atapeleka hua wawili au makinda mawili ya njiwa kwa kuhani penye lango la hema la mkutano. Kuhani atamtoa mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, naye atamfanyia upatanisho, kwa sababu alitenda dhambi kwa ajili ya maiti. Siku hiyohiyo, atakiweka wakfu kichwa chake na kujiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu kwa siku zake za kujitenga. Hizo siku za kwanza hazitahesabiwa kwa sababu nywele zake zilizokuwa zimewekwa wakfu zimetiwa unajisi. Atatoa mwanakondoo dume wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya hatia. “Hii ndiyo sheria ya mnadhiri wakati akisha kamilisha muda wake wa kujiweka wakfu: Ataletwa penye lango la hema la mkutano, na kumtolea Mwenyezi-Mungu zawadi zake: Mwanakondoo dume mmoja wa mwaka mmoja asiye na dosari kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; mwanakondoo jike mmoja wa mwaka mmoja asiye na dosari kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; na kondoo dume mmoja asiye na dosari kwa ajili ya sadaka ya amani. Pia atatoa kikapu cha mikate isiyotiwa chachu: Maandazi ya unga laini na mafuta, na mikate myembamba iliyopakwa mafuta pamoja na sadaka za nafaka na za kinywaji. “Kuhani atamtolea Mwenyezi-Mungu vitu vyote hivi pamoja na sadaka yake ya dhambi na sadaka yake ya kuteketezwa. Atamtolea Mwenyezi-Mungu huyo kondoo kama tambiko ya amani, atamtoa pamoja na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, sadaka ya nafaka na ya kinywaji. Hapo penye mlango wa hema la mkutano, mnadhiri huyo atanyoa nywele zake na kuzitia katika moto ulio chini ya tambiko ya sadaka ya amani. “Kisha kuhani atachukua bega la yule kondoo dume likiwa limechemshwa pamoja na andazi moja lililotiwa chachu kutoka kikapuni na mikate myembamba pia isiyotiwa chachu na kumpa mnadhiri mikononi akisha maliza kunyoa nywele zake alizokuwa nazo wakati wa kuwekwa wakfu. Halafu kuhani atavitikisa vitu hivyo kama sadaka ya kutikisa mbele ya Mwenyezi-Mungu; vyote hivi ni sehemu takatifu kwa kuhani, pamoja na kidari kilichotikiswa na paja lililotolewa kama sadaka. Baada ya hayo yote, mnadhiri anaweza kunywa divai. “Hiyo ndizo sheria inayomhusu mnadhiri anayeahidi kwa kiapo. Sadaka yake kwa Mwenyezi-Mungu ilingane na nadhiri yake, licha ya chochote kingine anachoweza kutoa; atafanya kulingana na nadhiri aliyoweka, kadiri ya sheria ya kujiweka wakfu kwake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mwambie Aroni na wanawe kwamba hivi ndivyo mtakavyowabariki Waisraeli: Mtawaambia, ‘Mwenyezi-Mungu awabariki na kuwalinda; Mwenyezi-Mungu awaangalie kwa wema, na kuwafadhili; Mwenyezi-Mungu awaoneshe wema wake na kuwapa amani.’ “Ndivyo watakavyotamka jina langu juu ya Waisraeli, nami nitawabariki.” Siku Mose alipomaliza kulisimamisha hema takatifu, kulimiminia mafuta na kuliweka wakfu pamoja na vyombo vyake vyote, kuimiminia mafuta na kuiweka wakfu madhabahu na vyombo vyake vyote, viongozi wa Israeli na wakuu wa koo na viongozi wa makabila ambao walisimamia watu wale waliohesabiwa, walimletea Mwenyezi-Mungu matoleo yao: Magari yaliyofunikwa sita na mafahali kumi na wawili, gari moja kwa kila viongozi wawili na fahali mmoja kwa kila kiongozi. Baada ya kuvitoa mbele ya hema takatifu, Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Pokea matoleo haya ili yatumiwe katika huduma itakayofanywa kwa ajili ya hema la mkutano, uwape Walawi, kila mmoja kwa kadiri ya kazi yake.” Basi, Mose akachukua magari na mafahali akawapa Walawi. Wagershoni wakapewa magari mawili na mafahali wanne, kwa kadiri ya huduma yao, na Wamerari wakapewa magari manne na mafahali wanane, kuwasaidia katika kazi zao zote chini ya uongozi wa Ithamari mwana wa kuhani Aroni. Lakini Mose hakuwapa chochote Wakohathi kwa kuwa wao walikuwa na jukumu la kutunza vitu vitakatifu ambavyo vilipaswa kubebwa mabegani. Viongozi hao wakatoa sadaka kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu siku ile ilipopakwa mafuta; walitoa sadaka zao mbele ya madhabahu. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Kila siku kiongozi mmoja atatoa sadaka yake kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu.” Basi, yule aliyetoa sadaka siku ya kwanza, alikuwa Nashoni mwana wa Aminadabu, wa kabila la Yuda. Sadaka yake ilikuwa: Sahani moja ya fedha yenye uzito wa kilo moja u nusu na birika moja la fedha lenye uzito wa gramu 800 kulingana na vipimo vya hema takatifu; sahani na birika hilo vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu chenye uzito wa gramu 110 kikiwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga; kondoo dume mmoja, na mwanakondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; na fahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo madume watano wa mwaka mmoja kwa ajili ya tambiko ya sadaka za amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Nashoni mwana wa Aminadabu. Siku ya pili, Nethaneli mwana wa Suari, kiongozi wa kabila la Isakari alitoa sadaka. Nethaneli alitoa: Sahani moja ya fedha ya kilo moja u nusu na bakuli moja la fedha la gramu 800 kulingana na vipimo vya hema takatifu, sahani na bakuli hilo vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya tambiko ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu cha gramu 110 kikiwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja, na mwanakondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; fahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo madume watano wa mwaka mmoja kwa ajili ya tambiko ya sadaka za amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Nethaneli mwana wa Suari. Siku ya tatu ikawa zamu ya Eliabu mwana wa Heloni, kiongozi wa kabila la Zebuluni. Sadaka yake ilikuwa: Sahani moja ya fedha ya kilo moja u nusu na bakuli moja la fedha la gramu 800, kulingana na vipimo vya hema takatifu, sahani na bakuli hilo vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu cha gramu 110 kikiwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja, na mwanakondoo dume wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; fahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo madume watano wa mwaka mmoja kwa ajili ya tambiko ya sadaka za amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Eliabu mwana wa Heloni. Siku ya nne ikawa zamu ya Elisuri mwana wa Shedeuri, kiongozi wa kabila la Reubeni. Sadaka yake ilikuwa: Sahani moja ya fedha ya kilo moja u nusu na bakuli moja la fedha la gramu 800, kulingana na vipimo vya hema takatifu, sahani na bakuli hili vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu cha gramu 110 kikiwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja, na mwanakondoo dume wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; fahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo madume watano wa mwaka mmoja kwa ajili ya tambiko ya sadaka za amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Elisuri mwana wa Shedeuri. Siku ya tano ikawa zamu ya Shelumieli mwana wa Suri-shadai, kiongozi wa kabila la Simeoni. Sadaka yake ilikuwa: Sahani moja ya fedha ya kilo moja u nusu na bakuli moja la fedha la gramu 800, kulingana na vipimo vya hema takatifu, sahani na bakuli vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha fedha cha gramu 110 kikiwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja, na mwanakondoo dume mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; na fahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo madume watano wa mwaka mmoja kwa ajili tambiko ya sadaka za amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Shelumieli mwana wa Suri-shadai. Siku ya sita ikawa zamu ya Eliasafu mwana wa Deuli, kiongozi wa kabila la Gadi. Sadaka yake ilikuwa: Sahani moja ya fedha ya kilo moja u nusu na bakuli moja la fedha la gramu 800, kulingana na vipimo vya hema takatifu, sahani na bakuli vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu cha gramu 110 kikiwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; na mafahali wawili, beberu watano, na wanakondoo madume watano wa mwaka mmoja kwa ajili ya tambiko ya sadaka za amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Eliasafu mwana wa Deuli. Siku ya saba ikawa zamu ya Elishama mwana wa Amihudi, kiongozi wa kabila la Efraimu. Sadaka yake ilikuwa: Sahani moja ya fedha ya kilo moja u nusu na bakuli moja la fedha la gramu 800, kulingana na vipimo vya hema takatifu, sahani na bakuli vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu cha gramu 110 kikiwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; mafahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo madume watano wa mwaka mmoja kwa ajili ya tambiko ya sadaka za amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Elishama mwana wa Amihudi. Siku ya nane ikawa zamu ya Gamalieli mwana wa Pedasuri, kiongozi wa kabila la Manase. Sadaka yake ilikuwa: Sahani moja ya fedha ya kilo moja u nusu, na bakuli la fedha la gramu 800, kulingana na vipimo vya hema takatifu, vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu cha gramu 110 kilichokuwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; mafahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo madume watano wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka za amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Gamalieli mwana wa Padasuri. Siku ya tisa ikawa zamu ya Abidani mwana wa Gideoni, kiongozi wa kabila la Benyamini. Sadaka yake ilikuwa: Sahani moja ya fedha ya kilo moja u nusu na bakuli moja la fedha la gramu 800, kulingana na vipimo vya hema takatifu, sahani na bakuli vilikuwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu cha gramu 110 kilichokuwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka kuondoa dhambi; fahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo madume watano wa mwaka mmoja kwa ajili ya tambiko ya sadaka ya amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Abidani mwana wa Gideoni. Siku ya kumi ikawa zamu ya Ahiezeri mwana wa Amishadai, kiongozi wa kabila la Dani. Sadaka yake ilikuwa: Sahani moja ya fedha ya kilo moja u nusu na bakuli moja la fedha la gramu 800, kadiri ya vipimo vya hema takatifu; sahani na bakuli vilikuwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu cha gramu 110 kilichokuwa kimejazwa ubani; fahali mmoja wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; fahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo madume watano wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Ahiezeri mwana wa Amishadai. Siku ya kumi na moja ikawa zamu ya Pagieli mwana wa Okrani, kiongozi wa kabila la Asheri. Sadaka yake ilikuwa: Sahani ya fedha ya kilo moja u nusu na bakuli moja la fedha la gramu 800 kadiri ya vipimo vya hema takatifu vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu cha gramu 110 kilichokuwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; fahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo wa mwaka mmoja watano kwa ajili ya kutoa tambiko ya sadaka ya amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Pagieli mwana wa Okrani. Na siku ya kumi na mbili ilikuwa zamu ya Ahira mwana wa Enani, kiongozi wa kabila la Naftali. Sadaka yake ilikuwa: Sahani moja ya fedha ya kilo moja u nusu na bakuli la fedha la gramu 800 kadiri ya vipimo vya hema takatifu; sahani na bakuli vikiwa vimejazwa unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka; kisahani kimoja cha dhahabu cha gramu 110 ambacho kilikuwa kimejazwa ubani; fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi; fahali wawili, kondoo madume watano, beberu watano na wanakondoo madume wa mwaka mmoja watano kwa ajili ya tambiko ya sadaka ya amani. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka ya Ahira mwana wa Enani. Jumla ya matoleo ya sadaka za viongozi wa Israeli kwa ajili ya madhabahu siku ilipowekwa wakfu ilikuwa: Sahani za fedha kumi na mbili, birika za fedha kumi na mbili, na visahani vya dhahabu kumi na viwili. Kila sahani ya fedha, ilikuwa yenye uzito wa kilo moja u nusu na kila kisahani kilikuwa chenye uzito wa gramu 800. Hivyo vyombo vyote vilikuwa na uzito wa kilo ishirini na saba na gramu 600 kadiri ya vipimo vya hema takatifu. Vile visahani vya dhahabu kumi na viwili vyenye kujaa ubani, kila kimoja kikiwa na uzito wa gramu 110 kadiri ya vipimo vya hema takatifu vilikuwa na jumla ya uzito wa kilo moja na gramu 320. Jumla ya wanyama wote wa sadaka ya kuteketezwa ilikuwa mafahali kumi na wawili, kondoo madume kumi na wawili, na wanakondoo madume wa mwaka mmoja kumi na wawili, pamoja na sadaka ya nafaka na beberu kumi na wawili kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, na kwa ajili ya tambiko ya sadaka ya amani, jumla ya wanyama waliotolewa ilikuwa mafahali ishirini na wanne, kondoo madume sitini, beberu sitini, na wanakondoo madume wa mwaka mmoja sitini. Hiyo ndiyo iliyokuwa sadaka iliyotolewa kwa ajili ya madhabahu, baada ya madhabahu hiyo kupakwa mafuta. Wakati Mose alipoingia ndani ya hema la mkutano ili kuongea na Mwenyezi-Mungu, alisikia sauti kutoka upande wa juu wa kiti cha rehema, kilichokuwa juu ya sanduku la agano, kutoka kati ya wale viumbe wawili wenye mabawa. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mwambie Aroni kwamba wakati atakapoziweka zile taa saba kwenye kinara, azipange ili ziangaze upande wa mbele wa kinara hicho.” Aroni akatii maagizo hayo, akaziweka taa hizo ili ziangaze upande wa mbele wa kinara, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Toka sehemu za juu mpaka chini kinara hicho cha taa kilikuwa kimetengenezwa kwa ustadi mkubwa kwa dhahabu iliyofuliwa kufuatana na mfano ambao Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwonesha Mose. Tena Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Watenge Walawi kutoka Waisraeli, uwatakase. Hivi ndivyo utakavyowatakasa: Wanyunyizie maji ya kutakasia kisha uwaambie wajinyoe mwili mzima, wafue nguo zao na kujitakasa. Kisha watatwaa fahali mmoja mchanga pamoja na sadaka yake ya nafaka, yaani unga laini uliochanganywa na mafuta; nawe utatwaa fahali mwingine mchanga kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi. Kisha utawakusanya watu wote wa Israeli na kuwaleta Walawi mbele ya hema la mkutano. Utakapowaleta Walawi mbele yangu, Waisraeli watawawekea Walawi mikono, halafu Aroni atawaweka hao mbele yangu kama sadaka ya kutikiswa kutoka kwa Waisraeli wanihudumie. Kisha Walawi wataweka mikono yao juu ya vichwa vya fahali hao; mmoja wao utamtoa kuwa sadaka ya kuondoa dhambi, na huyo mwingine utamtoa kuwa sadaka ya kuteketezwa inayotolewa kwangu, ili kuwafanyia upatanisho Walawi. “Kisha utawasimamisha Walawi mbele ya Aroni na wanawe na kuwaweka mbele yangu kama sadaka ya kutikiswa. Hivi ndivyo utakavyowatenga Walawi miongoni mwa Waisraeli wengine ili wawe wangu. Baada ya kuwatakasa Walawi na kuwatoa kama sadaka ya kutikiswa wataingia ili kuhudumu katika hema la mkutano. Hao wametolewa wawe wangu kabisa, badala ya wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli. Maana wazaliwa wote wa kwanza miongoni mwa Waisraeli ni wangu, wanadamu na wanyama; kwa sababu katika siku nilipowaua wazaliwa wote wa kwanza nchini Misri, niliwaweka wakfu kwangu. Sasa ninawachukua Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli, na nimempa hao Aroni na wanawe, kama zawadi kutoka kwa Waisraeli, ili wafanye kazi katika hema la mkutano kwa ajili ya Waisraeli na kuwafanyia upatanisho ili pasitokee pigo miongoni mwa Waisraeli wakikaribia mahali patakatifu.” Kwa hiyo Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawaweka wakfu Walawi, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Walawi wakajitakasa dhambi na kuzifua nguo zao, naye Aroni akawatoa kama sadaka ya kutikiswa mbele ya Mwenyezi-Mungu. Pia, Aroni alifanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa. Baada ya hayo Walawi waliingia na kufanya huduma yao katika hema la mkutano chini ya usimamizi wa Aroni na wanawe, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Kila Mlawi mwenye umri wa miaka ishirini na mitano na zaidi, atahudumu katika hema langu la mkutano; na kustaafu afikishapo umri wa miaka hamsini. Baada ya hapo, anaweza kuwasaidia Walawi wenzake wanapohudumu katika hema, lakini haruhusiwi kutoa huduma yoyote peke yake. Ndivyo utakavyowapangia kazi Walawi.” Kisha mnamo mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka Misri, Mwenyezi-Mungu aliongea na Mose katika jangwa la Sinai. Alimwambia: “Waisraeli sharti waiadhimishe sikukuu ya Pasaka wakati uliopangwa. Hii itakuwa siku ya kumi na nne ya mwezi huu; wakati wa jioni watafanya hivyo kufuatana na masharti na maagizo yake yote.” Kwa hiyo, Mose akawaambia watu kwamba wanapaswa kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka. Basi, wakaiadhimisha Pasaka jioni, siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, katika jangwa la Sinai. Waisraeli walifanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Lakini, baadhi ya watu waliokuwapo walikuwa hawawezi kuiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka kwa sababu walikuwa wamegusa maiti, wakawa najisi. Hao waliwaendea Mose na Aroni, wakawaambia, “Sisi tu najisi kwa kuwa tumegusa maiti, lakini kwa nini tukatazwe kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka zake kwa wakati uliopangwa pamoja na Waisraeli wengine?” Mose akawajibu, “Ngojeni mpaka hapo nitakapopata maagizo juu yenu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu.” Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mmoja wenu au mmoja wa wazawa wenu akiwa najisi kwa sababu amegusa maiti au akiwa mbali safarini, lakini akiwa anataka kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka, mtu kama huyo anaruhusiwa kufanya hivyo mwezi mmoja baadaye, jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Ataiadhimisha kwa kula mikate isiyotiwa chachu na mboga chungu. Wasibakize chakula chochote hadi asubuhi, wala wasivunje hata mfupa mmoja wa wanyama wa Pasaka. Wataiadhimisha sikukuu hii ya Pasaka kulingana na kanuni zake zote. Lakini mtu yeyote ambaye ni safi au hayumo safarini, asipoiadhimisha sikukuu ya Pasaka, atatengwa na watu wake kwa kuwa hakunitolea sadaka kwa wakati uliopangwa. Ni lazima aadhibiwe kwa ajili ya dhambi yake. “Ikiwa kuna mgeni anayeishi pamoja nanyi na anapenda kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka, mtu huyo sharti afanye hivyo kulingana na masharti na maagizo yote ya Pasaka. Kila mtu atafuata masharti yaleyale, akiwa mgeni au mwenyeji.” Siku ambayo hema takatifu lilisimikwa, wingu lilishuka na kulifunika hema la maamuzi. Wakati wa usiku wingu hilo lilionekana kama moto mpaka asubuhi. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kila siku; wingu lililifunika hema mchana, na usiku lilionekana kama moto. Kila mara wingu hilo lilipoinuliwa juu ya hema, Waisraeli walivunja kambi na kupiga kambi tena mahali wingu hilo lilipotua. Walisafiri kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, na kupiga kambi tena kwa amri yake. Muda wote wingu hilo lilipokuwa juu ya hema, watu walikaa katika kambi hiyo. Hata kama wingu hilo lilikaa juu ya hema kwa muda wa siku nyingi, Waisraeli walimtii Mwenyezi-Mungu, nao hawakuondoka. Wakati mwingine wingu hilo lilikaa juu ya hema kwa muda wa siku chache tu; lakini kila wakati Waisraeli walibaki kambini; walihama kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Wakati mwingine wingu lilikaa juu ya hema tangu jioni mpaka asubuhi tu; na mara tu lilipoinuliwa, hao watu pia walifunga safari. Na ikiwa lilikaa juu ya hema mchana kutwa na usiku kucha, wao waliondoka tu wingu lilipoinuliwa. Ikiwa ni siku mbili, mwezi, mwaka au zaidi, muda wote wingu hilo lilipokuwa juu ya hema, Waisraeli hawakuhama; lakini lilipoinuliwa, nao pia walihama. Kwa agizo la Mwenyezi-Mungu walipiga kambi na kwa agizo la Mwenyezi-Mungu walisafiri. Walishika agizo la Mwenyezi-Mungu kama alivyotoa amri yake kwa njia ya Mose. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Tengeneza tarumbeta mbili kwa fedha iliyofuliwa. Utazitumia tarumbeta hizo wakati wa kuwaita watu na wakati wa kuvunja kambi. Tarumbeta zote mbili zikipigwa pamoja, watu wote watakusanyika karibu nawe mbele ya lango la hema la mkutano. Lakini kama ikipigwa tarumbeta moja tu, basi ni viongozi tu wa makabila ya Israeli watakaokusanyika karibu nawe. Ishara hiyo ikitolewa kwa kupiga tarumbeta, wakazi wa kambi za mashariki wataanza safari. Ishara hiyo ikipigwa mara ya pili, wale wa kambi za upande wa kusini wataanza kuondoka. Ishara hiyo ya tarumbeta itatolewa kila wakati wa kuanza safari. Lakini wakati wa kuwaita watu wakusanyike pamoja, tarumbeta zitapigwa kwa njia ya kawaida. Wazawa wa Aroni, makuhani, ndio watakaopiga tarumbeta hizo. Utaratibu huo utafuatwa daima katika vizazi vyenu vyote. “Wakati wa vita nchini mwenu dhidi ya adui wanaowashambulia, mtatoa ishara ya vita kwa kupiga tarumbeta hizi ili Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu apate kuwakumbuka na kuwaokoa na adui zenu. Hali kadhalika katika siku zenu za furaha, kama vile sikukuu za mwandamo wa mwezi na sikukuu nyinginezo, mtazipiga tarumbeta hizi wakati mnapotoa sadaka zenu za kuteketezwa na tambiko za sadaka zenu za amani. Hapo mimi Mungu wenu nitawakumbukeni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Mnamo siku ya ishirini ya mwezi wa pili, mwaka wa pili tangu wana wa Israeli walipoondoka Misri, wingu lililokuwa juu ya hema la maamuzi liliinuliwa, nao Waisraeli wakaanza safari yao kutoka jangwa la Sinai. Wingu hilo lilipaa na hatimaye likatua katika jangwa la Parani. Kwa mara ya kwanza Waisraeli walifunga safari hiyo kwa amri ya Mwenyezi-Mungu kama ilivyotolewa na Mose. Wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi cha kabila la Yuda, walitangulia, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Nashoni mwana wa Aminadabu. Nethaneli mwana wa Suari, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Isakari. Naye Eliabu mwana wa Heloni, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Zebuluni. Kisha, hema lilishushwa, na watu wa ukoo wa Gershoni na wa Merari ambao walilibeba, walianza kuondoka. Halafu, watu waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Reubeni, walifuata kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri. Shelumieli mwana wa Suri-shadai, aliliongoza kabila la Simeoni. Naye Eliasafu mwana wa Deueli, aliliongoza kabila la Gadi. Kisha walifuata watu wa ukoo wa Kohathi, wakiwa wamebeba vyombo vitakatifu. Walipowasili, hema lilikuwa limekwisha simikwa. Baada ya hao, walifuata watu waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Efraimu, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Elishama mwana wa Amihudi. Gamalieli mwana wa Pedasuri aliliongoza kabila la Manase, naye Abidani mwana wa Gideoni, aliliongoza kabila la Benyamini. Mwisho, wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Dani, waliokuwa kama walinzi nyuma ya vikosi vyote, walisafiri, kundi moja baada ya jingine. Hawa waliongozwa na Ahiezeri mwana wa Amishadai. Pagieli, mwana wa Okrani, aliliongoza kabila la Asheri. Naye Ahira mwana wa Enani, aliliongoza kabila la Naftali. Huu basi, ndio utaratibu walioufuata Waisraeli kulingana na makundi yao, kila wakati walipovunja kambi na kuanza kusafiri tena. Mose alimwambia shemeji yake, Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwe wake, “Sisi tunasafiri kwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu amesema ‘Nitawapa nyinyi mahali hapo’. Basi, twende pamoja, nasi tutakutendea mema; maana Mwenyezi-Mungu ameahidi kutupa sisi Waisraeli fanaka.” Lakini Hobabu akajibu, “Mimi sitafuatana nanyi; ila nitarudi katika nchi yangu na kwa jamaa zangu.” Mose akamwambia, “Tafadhali usituache, maana wewe unajua mahali tunapoweza kupiga kambi jangwani, na unaweza kuwa kiongozi wetu. Tena ukiandamana nasi chochote chema atakachotutendea Mwenyezi-Mungu, ndicho utakachotendewa nawe pia.” Basi, watu wakasafiri toka Sinai, Mlima wa Mwenyezi-Mungu, mwendo wa siku tatu. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwatangulia mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupiga kambi. Kila waliposafiri kutoka kambi moja hadi nyingine, wingu la Mwenyezi-Mungu lilikuwa juu yao mchana. Kila wakati sanduku liliposafiri kwenda mbele, Mose alisema, “Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwatawanye adui zako, na hao wanaokuchukia uwafanye wakimbie kutoka mbele yako.” Na kila wakati liliposimama, Mose alisema, “Warudie, ee Mwenyezi-Mungu, hawa maelfu na maelfu ya Israeli.” Watu walianza kumlalamikia Mwenyezi-Mungu juu ya taabu zao. Mwenyezi-Mungu aliposikia, alishikwa na hasira, akawapelekea moto. Moto huo uliwaka kati yao na kuchoma upande mmoja wa kambi. Watu wakamlilia Mose, naye akamwomba Mwenyezi-Mungu na moto huo ukazimika. Kwa hiyo, mahali hapo pakaitwa Tabera, kwa sababu hapo moto wa Mwenyezi-Mungu uliwaka kati ya watu. Miongoni mwa Waisraeli kulikuwa na kundi fulani lililoandamana nao ambalo lilikuwa na hamu kubwa. Waisraeli kwa mara nyingine walilia, wakisema. “Laiti kama tungeweza kupata nyama ya kula! Tunakumbuka, samaki tuliokula kule Misri bila malipo, matango, matikiti, mboga, vitunguu na vitunguu saumu! Lakini sasa nguvu zimetuishia na hakuna chakula kingine isipokuwa hii mana tu!” Mana ilikuwa kama punje za mtama, rangi yake ilikuwa kama ya bedoza. Watu walizungukazunguka na kuikusanya, kisha waliisaga kwa mawe ya kusagia au waliitwanga kwa vinu, halafu waliitokosa vyunguni na kutengeneza maandazi. Ladha yake ilikuwa kama ya maandazi yaliyokaangwa kwa mafuta. (Umande ulipoanguka kambini wakati wa usiku, mana pia ilianguka pamoja na huo umande). Mose alisikia watu wakilia katika familia zote, kila mtu penye lango la hema lake. Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka sana; naye Mose alichukizwa. Ndipo Mose alipomwambia, Mwenyezi-Mungu “Kwa nini unanitendea vibaya mimi mtumishi wako? Mbona hupendezwi nami, kwa nini umenitwika mzigo wa kuwatunza watu wote hawa? Je, ni mimi niliyewazaa, hata ukaniambia niwabebe kifuani pangu kama mlezi abebavyo mtoto mchanga, na kuwapeleka mpaka nchi uliyoapa kuwapa babu zao? Nitapata wapi nyama ya kuwalisha watu hawa wote? Maana wanalia mbele yangu wakisema: ‘Tupe nyama tule!’ Siwezi kuwatunza watu wote hawa peke yangu; hilo ni jukumu kubwa mno kwangu! Ikiwa hivi ndivyo utakavyonitenda, afadhali uniue mara moja! Kama ninapata kibali mbele yako, usiniache niikabili taabu yangu.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Wakusanyeni wazee sabini wa Israeli, ambao wewe unajua wanaheshimiwa na kukubaliwa na watu kuwa viongozi, uwalete kwenye hema la mkutano, wasimame karibu nawe. Nitashuka huko na kuzungumza nawe; nitachukua sehemu ya roho niliyokupa, niwape watu hao. Nao watabeba jukumu la kuwatunza watu hawa pamoja nawe, usije ukaubeba mzigo huo peke yako. Sasa waambie watu hivi: Jitakaseni kwa ajili ya kesho; mtakula nyama. Mwenyezi-Mungu amesikia mkilia na kusema kuwa hakuna wa kuwapeni nyama, na kwamba hali yenu ilikuwa nzuri zaidi mlipokuwa Misri. Sasa Mwenyezi-Mungu atawapeni nyama, nanyi sharti muile. Mtakula nyama si kwa muda wa siku moja tu, au mbili, au tano, au kumi au ishirini, bali kwa muda wa mwezi mzima! Mtaila hadi iwatoke puani, mpaka muikinai. Yote hayo ni kwa sababu mmemkataa Mwenyezi-Mungu aliye hapahapa miongoni mwenu, na kulia mbele yake mkisema, ‘Kwa nini tulitoka Misri?’” Lakini Mose alimwambia Mwenyezi-Mungu, “Idadi ya watu ninaowaongoza hapa ni 600,000 waendao kwa miguu, nawe wasema, ‘Nitawapa nyama ya kuwatosha mwezi mzima!’ Je, panaweza kuchinjwa kondoo na ng'ombe wa kuwatosheleza? Je, samaki wote baharini wavuliwe kwa ajili yao?” Mwenyezi-Mungu akamjibu Mose, “Je, uwezo wangu umepungua? Utaona basi kama neno langu litakuwa la kweli kwako au la.” Basi, Mose akaenda na kuwajulisha watu yale aliyosema Mwenyezi-Mungu. Kisha, akakusanya wazee sabini kutoka miongoni mwa wazee viongozi nao akawaweka kandokando kuizunguka hema. Hapo, Mwenyezi-Mungu akashuka katika wingu na kuzungumza naye. Halafu akatwaa sehemu ya roho aliyokuwa amempa Mose, akawapa kila mmoja wa wale wazee sabini. Walipoingiwa na roho hiyo, wazee hao walianza kutoa unabii, lakini hawakurudia kufanya hivyo. Wazee wawili kati ya wale sabini waliochaguliwa, Eldadi na Medadi, walikuwa wamebaki kambini wenzao walipokwenda kwenye hema. Roho iliwajia humohumo kambini, wakaanza kutoa unabii mahali walipokuwa. Kijana mmoja alitoka mbio na kumwambia Mose, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.” Hapo, Yoshua, mwana wa Nuni, ambaye alikuwa msaidizi wa Mose tangu ujana wake, akamwambia Mose, “Bwana wangu, wakataze!” Lakini Mose akamjibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Laiti Mwenyezi-Mungu angewapa watu wake wote roho yake nao wakawa manabii!” Kisha Mose alirudi kambini pamoja na wale wazee sabini wa Israeli. Baadaye Mwenyezi-Mungu akavumisha upepo kwa ghafla, ukaleta kware kutoka baharini na kuwafanya watue kando ya kambi, mwendo wa siku moja hivi kila upande kuizunguka kambi, wakarundikana chini karibu kimo cha mita moja hivi. Basi, siku hiyo yote, kutwa kucha, na siku iliyofuata watu walishughulika kukusanya kware; hakuna mtu aliyekusanya chini ya kilo 1,000. Wakawaanika kila mahali kandokando ya kambi ili wawakaushe. Kulipokuwa bado kuna nyama kwa wingi na kabla watu hawajawamaliza kuila, Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia watu, akawapiga watu kwa pigo kubwa sana. Kwa hiyo mahali hapo palipewa jina Kibroth-hataava; kwa sababu huko ndiko walikowazika watu waliokuwa walafi. Kutoka hapo Kibroth-hataava watu walisafiri mpaka Haserothi, wakapiga kambi yao na kukaa huko. Kisha Miriamu na Aroni walianza kumsema vibaya Mose kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa. Wakasema, “Hivi kwani Mwenyezi-Mungu amezungumza kwa kumwagiza Mose peke yake? Je, hajazungumza nasi pia?” Mwenyezi-Mungu aliyasikia maneno hayo. (Mose alikuwa mtu mnyenyekevu kuliko watu wengine wote waliokuwa duniani.) Halafu ghafla, Mwenyezi-Mungu akawaambia Mose, Aroni na Miriamu, “Njoni katika hema la mkutano, nyinyi watatu.” Basi, wote watatu wakaenda kwenye hema la mkutano. Hapo Mwenyezi-Mungu akashuka katika nguzo ya wingu, akasimama kwenye mlango wa hema, akawaita Aroni na Miriamu. Wote wawili wakasogea mbele. Kisha Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Sikilizeni maneno yangu: Kama kuna nabii miongoni mwenu, mimi Mwenyezi-Mungu hujifahamisha kwake katika maono na kuongea naye katika ndoto. Lakini kumhusu mtumishi wangu Mose, hali ni tofauti kabisa. Yeye ana jukumu la kuwatunza watu wangu wote. Mimi huongea naye ana kwa ana, waziwazi na si kwa kutumia mafumbo. Yeye huliona umbo langu mimi Mwenyezi-Mungu. Kwa nini, basi, hamkuogopa kusema vibaya dhidi ya mtumishi wangu Mose?” Hapo Mwenyezi-Mungu akawaka hasira dhidi yao, akaondoka, akaenda zake. Wingu lilipoondoka juu ya hema la mkutano, Miriamu alionekana ana ukoma, mweupe kama theluji. Aroni alipogeuka na kumtazama Miriamu, alishangaa kuona kuwa ameshikwa na ukoma. Hapo, Aroni akamwambia Mose, “Ewe bwana wangu, usituadhibu kwa kuwa tumetenda mambo ya kipumbavu na kufanya dhambi. Usimfanye Miriamu awe kama mtu aliyezaliwa mfu, ambaye karibu nusu ya mwili wake umelika.” Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nakusihi, ee Mungu, umponye.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kama baba yake angemtemea mate usoni, je, hangeaibika kwa siku saba? Basi, mtoe nje ya kambi akae huko muda wa siku saba, kisha unaweza kumruhusu arudi kambini.” Kwa hiyo, Miriamu akafukuzwa nje ya kambi kwa muda wa siku saba. Watu hawakuanza tena safari hadi Miriamu aliporudishwa tena kambini. Baada ya hayo, watu walifanya safari kutoka Haserothi, wakapiga kambi katika jangwa la Parani. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tuma watu waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani ambayo ninawapa wana wa Israeli. Utatuma mtu mmoja kutoka katika kila kabila, na mtu huyo lazima awe kiongozi katika kabila lake.” Basi, kwa mujibu wa agizo la Mwenyezi-Mungu, Mose akatuma watu kutoka jangwa la Parani. Watu wote waliotumwa walikuwa viongozi wa makabila mbalimbali ya wana wa Israeli. Ifuatayo ndiyo orodha ya majina ya watu hao: Kabila la Reubeni, Shamua mwana wa Zakuri. Kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori. Kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune. Kabila la Isakari, Igali mwana wa Yosefu. Kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni. Kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu. Kabila la Zebuluni, Gadieli mwana wa Sodi. Kabila la Yosefu (yaani kabila la Manase), Gadi mwana wa Susi. Kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali. Kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli. Kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi. Kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki. Haya ndiyo majina ya watu ambao Mose aliwatuma kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani. Mose alimpa Hoshea mwana wa Nuni jina jipya, akamwita Yoshua. Alipowatuma kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani, Mose aliwaambia: “Nendeni juu kule Negebu, hadi kwenye nchi ya milima, mkaipeleleze nchi ilivyo. Chunguzeni pia kama watu wanaoishi humo ni wenye nguvu au dhaifu, wengi au wachache. Pelelezeni kama nchi hiyo ni nzuri au mbaya, na kama miji wanamoishi ni kambi au ni nyumba zilizozungukwa na ngome. Chunguzeni pia kama nchi yenyewe ni tajiri au maskini, ina miti au haina. Muwe na mioyo ya ujasiri na mnaporudi chukueni baadhi ya matunda ya nchi hiyo.” Hayo yalikuwa majira ya zabibu zianzapo kuiva. Basi, watu hao wakaenda na kuipeleleza nchi toka jangwa la Sini hadi Rehobu, karibu na njia ya kuingilia Hamathi. Walikwenda hadi Negebu wakapita mpaka mji wa Hebroni. Humo waliwakuta Waahimani, Washeshai na Watalmai, wazawa wa Anaki. (Mji wa Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko nchini Misri). Walipofika katika Bonde la Eshkoli, watu hao walikata shada la mzabibu lililokuwa na matunda mengi nalo lilibebwa na watu wawili juu ya mti. Walichukua pia makomamanga kadhaa na tini. Mahali hapo paliitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya shada ambalo watu hao wa Israeli walikata kutoka mahali hapo. Baada ya kuipeleleza nchi kwa muda wa siku arubaini, watu hao walirudi. Waliwaendea Mose, Aroni na jumuiya ya Waisraeli huko Kadeshi, katika jangwa la Parani, wakatoa taarifa ya mambo waliyoyaona na kuwaonesha matunda ya nchi. Walimwambia Mose, “Tuliifikia nchi uliyotutuma tuipeleleze; hiyo ni nchi inayotiririka maziwa na asali, na hili ni tunda lake. Lakini wenyeji wake ni wenye nguvu sana, na miji yao ni imara na mikubwa sana. Zaidi ya hayo, huko tuliona wazawa wa Anaki. Waamaleki wanakaa katika eneo la Negebu; Wahiti, Wayebusi na Waamori wanakaa katika eneo la milima, na Wakanaani wanakaa karibu na bahari ya Mediteranea na karibu na kingo za mto Yordani.” Lakini Kalebu aliwanyamazisha watu mbele ya Mose, akasema, “Twende mara moja tukaimiliki nchi hiyo. Kwa kuwa tunao uwezo sana wa kushinda.” Lakini watu walioandamana naye kuipeleleza nchi wakasema, “Hatutaweza kupigana na watu hao; wao wana nguvu kuliko sisi.” Kwa hiyo wakaeneza mambo ya uongo kati ya wana wa Israeli kuhusu nchi waliyoipeleleza, wakisema, “Nchi hiyo inawaua watu wake. Pia watu wote tuliowaona huko ni wakubwa sana. Tuliona majitu huko, wazawa wa Anaki. Sisi tulijiona kuwa kama panzi mbele yao, na ndivyo walivyotuona sisi.” Jumuiya yote ya Waisraeli ikaangua kilio kikubwa, watu wakalia usiku ule. Waliwalalamikia Mose na Aroni wakisema, “Afadhali tungefia Misri! Afadhali tungefia papa hapa jangwani! Kwa nini Mwenyezi-Mungu anatupeleka katika nchi hiyo? Tutauawa vitani, na wake zetu na watoto wetu watachukuliwa mateka! Si afadhali turudi Misri?” Basi wakaanza kuambiana, “Na tuchague kiongozi, turudi Misri.” Hapo, Mose na Aroni wakaanguka kifudifudi mbele ya jumuiya yote ya Waisraeli. Yoshua, mwana wa Nuni, na Kalebu, mwana wa Yefune, ambao walikuwa miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi, wakazirarua nguo zao na kuiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Nchi tuliyokwenda kuipeleleza ni nzuri kupita kiasi. Ikiwa Mwenyezi-Mungu amependezwa nasi, atatupeleka huko na kutupa nchi inayotiririka maziwa na asali. Mradi tu msimwasi Mwenyezi-Mungu, wala msiwaogope wenyeji wa nchi hiyo. Maana wao ni mboga tu kwetu; kinga yao imekwisha ondolewa kwao, naye Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi; msiwaogope!” Lakini jumuiya yote ikatishia kuwapiga mawe. Ghafla, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatokea juu ya hema la mkutano, mbele ya Waisraeli wote. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Watu hawa watanidharau mpaka lini? Na, mpaka lini wataendelea kutoniamini, hata pamoja na miujiza yote niliyotenda kati yao? Nitawapiga kwa maradhi mabaya na kuwatupilia mbali; lakini, kutokana nawe, nitaunda taifa lingine kubwa, lenye nguvu kuliko wao.” Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Uliwatoa watu hawa nchini Misri kwa nguvu yako. Wamisri watakaposikia kwamba umewatenda hivyo watu wako, watawapasha habari wakazi wa nchi hii. Maana watu hawa wamekwisha pata habari kwamba wewe, ee Mwenyezi-Mungu, u pamoja nasi; maana wewe, ee Mwenyezi-Mungu, unaonekana waziwazi wingu lako linaposimama juu yetu, na kwamba wewe hututangulia mchana kwa nguzo ya wingu na usiku kwa nguzo ya moto. Sasa basi, ukiwaua watu wako wote kwa mara moja, mataifa ambayo yamekwisha sikia sifa zako yatasema, ‘Mwenyezi-Mungu aliwaua watu wake jangwani kwa sababu alishindwa kuwapeleka katika nchi aliyoahidi kuwapa.’ Basi, sasa nakusihi, ee Mwenyezi-Mungu, utuoneshe uwezo wako kwa kufanya kama ulivyotuahidi uliposema, ‘Mimi Mwenyezi-Mungu si mwepesi wa hasira, ni mwenye fadhili nyingi, na ni mwenye kusamehe uovu na makosa. Lakini kwa vyovyote vile sitakosa kuwaadhibu watoto na wajukuu hadi kizazi cha tatu na cha nne kwa dhambi za wazazi wao.’ Nakusihi uwasamehe watu hawa dhambi zao, kadiri ya fadhili zako nyingi kama vile ulivyowasamehe tangu watoke Misri hadi sasa.” Mwenyezi-Mungu akajibu, “Nimewasamehe kama ulivyoomba. Lakini kwa kweli, kama niishivyo na kadiri dunia itakavyojaa utukufu wangu, hakuna hata mmoja wao ambaye amewahi kuuona utukufu wangu na miujiza yangu niliyoifanya Misri na jangwani kisha akazidi kunijaribu mara hizi zote bila ya kutii sauti yangu, ataiona nchi ile niliyoapa kuwapatia babu zao; kadhalika hata wale wanaonidharau pia hawataiona. Bali kwa sababu mtumishi wangu Kalebu ni tofauti, na amenitii kikamilifu, nitamfikisha kwenye nchi hiyo aliyoingia na wazawa wake wataimiliki. Kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani wanakaa katika mabonde ya nchi hiyo, kesho geukeni nyuma mwende jangwani kuelekea bahari ya Shamu.” Kisha Mwenyezi-Mungu akamwuliza Mose na Aroni, “Kundi hili la watu waovu litaendelea kuninungunikia mpaka lini? Nimechoka na haya manunguniko ya Waisraeli juu yangu! Sasa wajibu hivi: Kama niishivyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, nitawatendeeni yaleyale niliyosikia mkiyasema: Mtakufa na miili yenu itatupwa humuhumu jangwani, kwa sababu mmenungunika dhidi yangu, hakuna hata mmoja wenu mwenye umri wa kuanzia miaka ishirini na zaidi, atakayeingia katika nchi hiyo ambayo niliapa kuwapa iwe yenu, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. Nyinyi mlisema kuwa watoto wenu watatekwa nyara, lakini mimi nitawafikisha watoto wenu kwenye nchi mliyoidharau, ili waijue na iwe makao yao. Lakini nyinyi, mtafia humuhumu jangwani. Watoto wenu watatangatanga na kutaabika humu jangwani kwa muda wa miaka arubaini kwa ajili ya ukosefu wenu wa imani mpaka mtu wenu wa mwisho atakapofia jangwani. Kutokana na makosa yenu, mtataabika kwa muda wa miaka arubaini, sawa na zile siku arubaini mlizopeleleza ile nchi, mwaka mmoja kwa kila siku moja; mtatambua kwamba mimi nimechukizwa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema: Hakika nitawatenda hivyo nyinyi nyote mliokusanyika hapa kunipinga. Wote wataishia humuhumu jangwani na ni humu watakamofia.” Wale watu ambao Mose aliwatuma kwenda kuipeleleza ile nchi waliorudi na kusababisha watu wamnungunikie Mwenyezi-Mungu kwa kuleta taarifa mbaya dhidi ya nchi, watu hao waliotoa taarifa ya uovu kuhusu hiyo nchi, walikufa kwa pigo mbele ya Mwenyezi-Mungu. Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, walibaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi. Naye Mose aliwaambia Waisraeli wote nao walilia kwa uchungu mwingi. Kesho yake, waliamka alfajiri na mapema wakaenda sehemu za milimani, wakisema, “Sasa tuko tayari kabisa kwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu alituahidi. Tunakiri kwamba tulitenda dhambi.” Lakini Mose akasema, “Sasa mbona mnavunja agizo la Mwenyezi-Mungu? Hivyo hamtafaulu! Msiende huko milimani msije mkapigwa bure na adui zenu, maana, Mwenyezi-Mungu hayuko pamoja nanyi. Mkiwakabili Waamaleki na Wakanaani, mtafia vitani; kwa kuwa mmeacha kumfuata Mwenyezi-Mungu, yeye hatakuwa pamoja nanyi.” Hata hivyo, wao walisisitiza kwenda juu milimani, ingawa sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, wala Mose hakuondoka kambini. Ndipo Waamaleki na Wakanaani, waliokuwa wakiishi katika nchi hiyo ya milima, wakashuka, wakawashambulia na kuwashinda. Wakawafukuza mpaka mji wa Horma. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli kwamba mtakapofika katika nchi ninayowapeni ambamo mtaishi, mkanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka kutoka katika mifugo yenu, sadaka ya kuteketezwa au tambiko, ili mtu atimize nadhiri aliyoweka au kutoa sadaka ya hiari au sadaka ya wakati wa sikukuu zenu zilizowekwa, na kufanya harufu nzuri ya kunipendeza mimi Mwenyezi-Mungu, basi, yule atoaye sadaka yake, atamletea pia Mwenyezi-Mungu sadaka ya nafaka ya kilo moja ya unga laini uliokandwa na kuchanganywa na lita moja ya mafuta; pamoja na divai ya sadaka ya kinywaji, lita moja, vitu hivyo vitaandamana na kila mnyama wa tambiko ya kuteketezwa: Kondoo au mbuzi. Wakati wa kutoa sadaka ya kondoo dume, kilo mbili za unga uliokandwa na lita moja u nusu ya mafuta vitatolewa kama sadaka ya nafaka, pamoja na sadaka ya kinywaji ya lita moja u nusu ya divai, na kufanya harufu nzuri ya sadaka haya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Wakati mtakapomtolea Mwenyezi-Mungu fahali kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa au tambiko ili kutimiza nadhiri au kwa ajili ya sadaka za amani, mtu atamtoa kama sadaka pamoja na sadaka ya nafaka ya unga wa kilo tatu ulio mzuri na lita 2 za mafuta, pamoja na sadaka ya kinywaji ya lita 2 za divai, na kufanya harufu nzuri ya sadaka ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. “Hivyo ndivyo vitu vitakavyotolewa pamoja na kila fahali, kondoo dume au mbuzi. Hesabu ya vitu hivyo itaongezwa kulingana na hesabu ya wanyama watakaotolewa. Kila mwananchi Mwisraeli atafuata maagizo hayo wakati anapotoa tambiko, harufu impendezayo Mwenyezi-Mungu. Na kama kuna mgeni anayeishi pamoja nanyi kwa muda au daima, akitaka kutoa sadaka yake kwa kuiteketeza, harufu impendezayo Mwenyezi-Mungu, mtu huyo atafanya kama mnavyofanya nyinyi. Katika vizazi vyote vijavyo, kanuni zilezile mtakazofuata nyinyi ndizo atakazofuata mgeni yeyote atakayeishi pamoja nanyi; mbele ya Mwenyezi-Mungu mtakuwa sawa; nyinyi na yeye mtakuwa chini ya sheria ileile moja na maagizo yaleyale.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waeleze Waisraeli kwamba wakati watakapoingia katika nchi ninayowapeleka kila mtakapokula mazao ya nchi hiyo, mtatenga kiasi fulani na kunipa mimi Mwenyezi-Mungu. Mtakapooka mikate, mkate wa kwanza wa mazao ya kwanza ya nafaka yenu utatolewa kama sadaka kutoka mahali pa kupuria nafaka. Mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka hii maalumu katika vizazi vyenu vyote vijavyo. “Lakini ikiwa mtakosa kuzifuata amri zote ambazo mimi Mwenyezi-Mungu nimewapa kwa njia ya Mose, kama siku zijazo watu hawatafuata yote ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nimemwamuru Mose, basi, ikiwa kosa hilo limefanyika bila kukusudia, bila jumuiya kujua, jumuiya yote itatoa fahali mmoja mchanga kuwa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu, pamoja na sadaka yake ya nafaka na ya divai kufuatana na maagizo yake. Kadhalika watu watatoa beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi. Kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya jumuiya yote ya Waisraeli, nao watasamehewa kwa sababu si kosa lililokusudiwa, na wameleta sadaka yao, sadaka ya kuteketeza kwa Mwenyezi-Mungu kama tambiko na sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya kosa lao. Jumuiya yote ya Waisraeli, pamoja na wageni wanaoishi nao, watasamehewa kwa sababu wote walihusika na kosa hilo. “Mtu mmoja akifanya dhambi bila kujua, atatoa mbuzi jike wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi. Kuhani atafanya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya huyo mtu aliyekosa bila kujua, naye atasamehewa. Mtafuata sheria moja kila mtu atakayekosea bila kukusudia, awe ni mwananchi Mwisraeli au ni mgeni anayeishi pamoja nanyi. “Lakini mtu yeyote atakayekosa kwa makusudi, awe mwananchi au mgeni, atakuwa anamdhihaki Mwenyezi-Mungu, na ni lazima akatiliwe mbali miongoni mwa watu wake. Maana amekataa yale aliyosema Mwenyezi-Mungu na kuvunja mojawapo ya amri zake. Mtu huyo atakatiliwa mbali kabisa; na lawama ya kifo chake itakuwa juu yake mwenyewe.” Siku moja, wakati Waisraeli walipokuwa jangwani, walimwona mtu mmoja akiokota kuni siku ya Sabato. Basi, mtu huyo akapelekwa mbele ya Mose, Aroni na jumuiya yote. Wao wakamweka kifungoni kwa sababu haikuwa bado imesemwa wazi namna ya kumfanya mtu wa namna hiyo. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mtu huyo lazima auawe; jumuiya yote itampiga mawe nje ya kambi.” Basi, watu wakamtoa nje ya kambi, wakampiga mawe mpaka akafa, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose: “Waambie watu wa Israeli, uwaagize wajifanyie vishada katika ncha za mavazi yao, na kutia nyuzi za buluu juu ya kila kishada. Waambie wafanye hivyo katika vizazi vyao vyote vijavyo. Vishada hivyo vitakuwa kumbukumbu kwenu. Kila mtakapoviona, mtazikumbuka amri zangu zote na kuzifuata, ili msije mkafuata matakwa yenu na yale mnayoyaona kwa macho yenu wenyewe. Vishada hivyo vitawakumbusha amri zangu zote na mtazifuata zote kikamilifu, nanyi mtakuwa watakatifu wangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa nchini Misri ili niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Baadaye Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu pamoja na watu watatu wa ukoo wa Reubeni: Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, hao wote waliungwa mkono na viongozi mashuhuri 250 waliochaguliwa na jumuiya yote, wakamwasi Mose. Walikusanyika mbele ya Mose na Aroni, wakawaambia, “Nyinyi mmepita kikomo! Jumuiya yote ni takatifu na kila mtu katika jumuiya hii ni mtakatifu, na Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi sote. Mbona sasa nyinyi mnajifanya wakuu wa jumuiya ya Mwenyezi-Mungu?” Mose aliposikia hayo, alijitupa chini kifudifudi. Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake, “Kesho asubuhi, Mwenyezi-Mungu ataonesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, naye atakayemchagua, atamwezesha kukaribia madhabahuni. Basi, fanyeni hivi: Asubuhi, wewe pamoja na wafuasi wako, mtachukua vyetezo, mweke makaa ya moto ndani na kutia ubani juu yake, kisha mtavipeleka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Halafu tutaona ni nani aliyechaguliwa na Mwenyezi-Mungu. Nyinyi Walawi mmepita kikomo!” Mose akaendelea kumwambia Kora, “Sikilizeni, enyi Walawi! Je, mnaona ni jambo dogo kwenu kwamba Mungu wa Israeli amewateua nyinyi miongoni mwa jumuiya ya Israeli, ili muweze kumkaribia, mhudumie katika hema la Mwenyezi-Mungu na kuihudumia na kuitumikia jamii yote? Amewatunukia heshima ya kuwa karibu naye, nyinyi pamoja na Walawi wenzenu wote. Sasa mnataka kunyakua hata ukuhani? Kwa hiyo wewe na kundi lako mnamshambulia Mwenyezi-Mungu. Nyinyi mnamnungunikia Aroni, lakini ukweli ni kwamba mnanungunika dhidi ya Mungu.” Mose alituma ujumbe kwa Dathani na Abiramu wana wa Eliabu ili waitwe, lakini wao wakasema, “Hatutakuja! Je, ni jambo dogo kwamba umetutoa Misri, nchi inayotiririka maziwa na asali, ili uje kutuua humu jangwani? Tena, unajifanya mkuu wetu! Zaidi ya hayo, hukutuleta kwenye nchi inayotiririka maziwa na asali, wala kutupatia urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Unafikiri utawafanya hawa watu kuwa vipofu? Hatutakuja!” Mose alikasirika mno, akamwambia Mwenyezi-Mungu “Usizikubali sadaka za watu hawa. Mimi sijachukua punda wa mtu yeyote, wala sijamdhuru mtu!” Mose akamwambia Kora, “Kesho usikose kuja pamoja na wafuasi wako mbele ya Mwenyezi-Mungu. Aroni pia atakuwapo. Kila mmoja wenu achukue chetezo chake, na kutia ubani, kisha atakipeleka mbele ya Mwenyezi-Mungu; kwa jumla vitakuwa vyetezo 250; wewe pia na Aroni, kila mmoja atakuwa na chetezo chake.” Basi, kila mmoja wao akachukua chetezo chake, akatia makaa ya moto na ubani, kisha wakaenda na kusimama mlangoni mwa hema la mkutano, pamoja na Mose na Aroni. Naye Kora akawakusanya watu wote pamoja, wakasimama mbele ya Mose na Aroni ambao walikuwa mlangoni mwa hema la mkutano. Ndipo utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukawatokea watu wote! Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Jitengeni na watu hawa, niwaangamize sasa hivi.” Lakini Mose na Aroni wakajitupa chini kifudifudi na kusema, “Ee Mwenyezi-Mungu uliye asili ya uhai wa binadamu wote. Je, mtu mmoja akikukosea, utaikasirikia jumuiya nzima?” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie watu waondoke karibu na makao ya hema ya Kora, Dathani na Abiramu.” Basi, Mose akaenda kwa Dathani na Abiramu, akifuatwa na wazee wa Israeli. Alipofika, akawaambia watu, “Tafadhalini ondokeni kwenye hema za watu hawa waovu na msiguse kitu chao chochote, msije mkaangamizwa pamoja nao kwa sababu ya dhambi zao zote.” Watu wakaondoka kwenye makao ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu wakatoka mahemani mwao na kusimama mlangoni wakiandamana na wake zao na watoto wao wote hata wale wanaonyonya. Hapo Mose akawaambia watu, “Hivi ndivyo mtakavyotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyenituma kufanya mambo haya yote, wala siyo kwa matakwa yangu mwenyewe. Watu hawa wakifa kifo cha kawaida, au wakipatwa na maafa kama watu wengine, basi jueni kuwa Mwenyezi-Mungu hakunituma. Lakini Mwenyezi-Mungu akifanya jambo ambalo halijapata kutendeka, ardhi ikafunuka na kuwameza watu hawa pamoja na kila kitu chao, wakaenda kuzimu wakiwa hai, basi mtajua kuwa watu hawa wamemdharau Mwenyezi-Mungu.” Mara tu alipomaliza kusema maneno hayo yote, ardhi chini ya Dathani na Abiramu ikafunuka kuwameza watu hao, jamaa zao, pamoja na wafuasi wote wa Kora na mali zao zote. Basi, wao, pamoja na vyote vilivyokuwa vyao wakashuka kuzimu hali wangali hai. Ardhi ikawafunika, wote wakatoweka. Waisraeli wote wengine waliokuwa karibu waliposikia vilio vyao walikimbia wakisema, “Tukimbie, ardhi isije ikatumeza na sisi pia.” Kisha Mwenyezi-Mungu akapeleka moto ukawateketeza wale watu 250 waliokwenda kufukiza ubani. Baada ya hayo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Aroni avitoe hivyo vyetezo penye moto, akautapanye mbali moto uliomo ndani, maana vyetezo hivyo ni vitakatifu. Vimekuwa vitakatifu kwa sababu watu hawa walivileta madhabahuni pa Mwenyezi-Mungu. Basi, vichukue vyetezo vya watu hao waliouawa kwa sababu ya dhambi zao, vifuliwe kuwa vyembamba ili viwe kifuniko cha madhabahu. Hili litakuwa onyo kwa Waisraeli wote.” Basi, kuhani Eleazari alivichukua vyetezo hivyo vya shaba ambavyo vililetwa mbele ya Mwenyezi-Mungu na wale watu walioteketezwa vikafuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu. Hili lilikuwa onyo kwa Waisraeli kwamba mtu yeyote ambaye si kuhani, yaani asiye wa ukoo wa Aroni asiende madhabahuni kumfukizia Mwenyezi-Mungu ubani. La sivyo ataangamizwa kama Kora na wafuasi wake. Haya yote yalitendeka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Eleazari kwa njia ya Mose. Kesho yake, Waisraeli wote walimnungunikia Mose na Aroni wakisema, “Mmewaua watu wa Mwenyezi-Mungu.” Walipokusanyika mbele ya Mose na Aroni ili kutoa malalamiko yao, waligeuka kuelekea hema la mkutano, wakaona kuwa wingu limeifunika hema na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa umetokea hapo. Mose na Aroni walikwenda, wakasimama mbele ya hema la mkutano, na Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Jitenge na watu hawa, niwaangamize mara moja!” Lakini wao wakajitupa chini kifudifudi. Mose akamwambia Aroni, “Chukua chetezo chako, kitie moto na kukiweka kando ya madhabahu, kisha ukitie ubani halafu uende nacho haraka kwa watu na kuwafanyia upatanisho. Fanya haraka! Ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imekwisha wafikia na pigo limeanza kuwashambulia.” Basi, Aroni akafanya kama alivyoambiwa na Mose. Alichukua chetezo chake na kukimbia hadi katikati ya watu waliokuwa wamekusanyika pamoja. Alipoona kwamba pigo limekwisha anza, alitia ubani katika chetezo na kuwafanyia watu upatanisho. Alipofanya hivyo, pigo hilo lilikoma, naye akabaki katikati ya waliokufa na walio hai. Idadi ya watu waliokufa kwa pigo ilikuwa 14,700, bila kuhesabu wale waliokufa kutokana na uasi wa Kora. Pigo lilipokoma, Aroni alirudi kwa Mose mlangoni mwa hema la mkutano. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli wakuletee fimbo kumi na mbili, kila kiongozi wa kabila fimbo moja. Liandike jina la kila mmoja wao kwenye fimbo yake, na jina la Aroni liandike juu ya fimbo inayowakilisha kabila la Lawi. Patakuwa na fimbo moja kwa kila kiongozi wa kabila. Zichukue fimbo hizo katika hema la mkutano na kuziweka mbele ya sanduku la agano, mahali ambapo mimi hukutana nawe. Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipua. Kwa njia hii nitayakomesha manunguniko ya Waisraeli juu yenu.” Mose akaongea na watu wa Israeli. Viongozi wao wote wakampa kila mmoja fimbo yake kulingana na kabila lake jumla zikawa fimbo kumi na mbili. Fimbo ya Aroni iliwekwa pamoja na fimbo hizo. Mose akaziweka fimbo hizo zote mbele ya Mwenyezi-Mungu katika hema la mkutano. Kesho yake asubuhi, Mose alikwenda katika hema la mkutano. Humo, aliikuta fimbo ya Aroni wa kabila la Lawi, imechipua na kutoa vichipukizi vilivyochanua maua na kuzaa matunda mabivu ya mlozi. Kisha Mose akazitoa fimbo zote hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawaonesha Waisraeli wote, na kila kiongozi akachukua fimbo yake. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Irudishe fimbo ya Aroni mbele ya sanduku la agano. Hiyo itatunzwa mahali hapo, na ni onyo kwa waasi hao kwamba wasipoacha kuninungunikia, watakufa.” Mose akafanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Waisraeli wakamwambia Mose, “Angalia sasa! Tunaangamia! Tumekwisha! Sote tumekwisha. Kila mtu atakayekaribia, hema la Mwenyezi-Mungu atakufa. Je, tutaangamia sote?” Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Lawama zote kuhusu huduma ya hema takatifu, zitakuwa juu yako, wanao na ukoo wako; kadhalika makosa yanayoambatana na ukuhani wako wewe mwenyewe na wanao mtahusika. Wewe, wanao na wazawa wako wote mtahudumu kama makuhani; jamaa zako wengine wa kabila lako watafanya kazi pamoja nawe mbele ya hema la maamuzi. Wao watafanya kazi utakazowapa na kutimiza wajibu wao kuhusu hema. Lakini hawana ruhusa kuvigusa vyombo vya hema, wala kuikaribia madhabahu, wasije wakafa, nawe pia ukafa. Wao watajiunga nawe kazini na kutimiza wajibu wao kikamilifu kuhusu huduma zote za hema, na wala pasiwe na mtu mwingine atakayekukaribia humo. Nyinyi mtafanya huduma za mahali patakatifu na madhabahu, ili ghadhabu yangu isije ikawatokea tena Waisraeli. Ni mimi niliyewachagua ndugu zenu Walawi miongoni mwa Waisraeli kama toleo kwenu. Wao wametengwa kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu, ili watoe huduma katika hema la mkutano. Lakini wewe peke yako na wanao mtatoa huduma zote za kikuhani kwa ajili ya madhabahu na vyote vilivyomo katika mahali patakatifu. Huo ni wajibu wenu, kwa sababu ninawapeni kipawa cha ukuhani. Mtu yeyote asiyestahili atakayevikaribia vyombo vya hema, atauawa.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Ninakukabidhi matoleo waliyonipa Waisraeli, vitu vyote vitakatifu walivyonipa: Vitu vyote vilivyowekwa wakfu na Waisraeli. Ninakupa vitu vyote wewe na wazawa wako kuwa fungu lenu, na hiyo ni haki yenu milele. Kati ya vitu vitakatifu kabisa ambavyo haviteketezwi motoni, hivi vitakuwa vyenu: Sadaka za nafaka, sadaka za kuondoa dhambi na sadaka za hatia. Kila kitu watu watakachonitolea kama tambiko takatifu kitakuwa chako na wanao. Mtavila vitu hivyo kama vitu vitakatifu kabisa, na ni wanaume tu ndio watakaovila; vitu hivyo ni vitakatifu kwenu. “Pia, vitu vingine vyote watakavyonitolea Waisraeli kama sadaka za kutikisa, vitakuwa vyako. Ninakupa wewe, wanao na binti zako kuwa haki yenu milele. Mtu yeyote katika jamaa yako asiye najisi anaweza kula vitu hivyo. “Ninakupa vitu vyote vizuri vinavyotokana na malimbuko ambayo Waisraeli hunitolea: Mafuta safi, divai na nafaka. Mazao yote ya kwanza ya matunda mabivu ya mashamba yao ambayo wataniletea mimi, yatakuwa yako. Kila mtu asiye najisi katika jamaa yako anaweza kula. Kila kitu kilichowekwa wakfu nchini Israeli kitakuwa chenu. “Kila mzaliwa wa kwanza ambaye Waisraeli watanitolea, akiwa mzaliwa wa kwanza wa binadamu, au wa mnyama, atakuwa wako. Walakini huna budi kuwakomboa wazaliwa wa kwanza wote wa binadamu, na kila mzaliwa wa kwanza wa mnyama aliye najisi ni lazima akombolewe. Wazaliwa hao wa kwanza watakombolewa wakiwa wenye umri wa mwezi mmoja kwa kulipiwa fedha shekeli tano, kulingana na vipimo vya hema takatifu. Lakini wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe, kondoo au mbuzi wasikombolewe; hao ni watakatifu. Damu yao utainyunyizia madhabahu na mafuta yao utayateketeza kuwa sadaka ya kuteketezwa ambayo ni harufu nzuri inipendezayo mimi Mwenyezi-Mungu. Nyama yao unaweza kuila, kama vile kidari na mguu wa nyuma wa kulia vinavyotolewa kama sadaka ya kutikisa. “Ninakupa wewe, wanao na binti zako, vitu vyote ambavyo watu wa Israeli hunitolea; hivyo ni haki yenu daima. Hili ni agano la milele mbele yangu ambalo ni kwa ajili yako na wazawa wako.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Wewe hutakuwa na urithi wowote katika nchi yao, wala kuwa na fungu lako miongoni mwao; mimi ndimi fungu lako na urithi wako kati ya Waisraeli.” “Kuhusu Walawi, hao nimewapa zaka zote ambazo Waisraeli hunitolea kuwa urithi wao. Haya yatakuwa malipo yao kwa huduma wanayotoa katika kulitunza hema langu la mkutano. Na tangu sasa, watu wengine wa Israeli wasilikaribie hema la mkutano wasije wakatenda dhambi na kujiletea kifo. Lakini Walawi peke yao ndio watakaohudumu katika hema la mkutano; na kuwajibika kikamilifu juu yake. Hili ni sharti la kudumu katika vizazi vyenu vyote. Walawi hawatakuwa na mali ya kurithi nchini Israeli, kwa sababu zaka wanazonitolea Waisraeli nimewapa kuwa urithi wao. Ndio maana nimesema kwamba wao hawatakuwa na urithi kati ya Waisraeli.” Kisha, Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Tena utawaambia Walawi maagizo yafuatayo: Wakati mtakapopokea zaka ambayo Mwenyezi-Mungu amewapa kutoka kwa Waisraeli iwe urithi wenu, mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sehemu moja ya kumi ya zaka hiyo. Sadaka hii yenu itakubaliwa kuwa kama malimbuko ya nafaka au kama zabibu anazonitolea mkulima. Basi, ndivyo mtakavyonitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za zaka mtakazopokea kutoka kwa Waisraeli. Zaka hiyo mtakayonitolea mimi Mwenyezi-Mungu mtampa kuhani Aroni. Kutokana na matoleo yote mtakayopokea, mtamtolea Mwenyezi-Mungu zaka ya sehemu iliyo bora kuliko zote na takatifu. Kwa hiyo utawaambia: Mkishanitolea sehemu bora kuliko zote, sehemu itakayobakia itakuwa yenu, kama ilivyo kwa mkulima ambaye huchukua kinachobakia baada ya kutoa sadaka zake za mazao ya kwanza ya nafaka na zabibu. Nanyi mtakula kilichotolewa mkiwa mahali popote pale pamoja na jamaa zenu maana ni ujira wenu kwa sababu ya huduma yenu katika hema la mkutano. Hamtakuwa na hatia yoyote mkila vitu hivyo, iwapo kama mmemtolea Mwenyezi-Mungu sehemu bora kuliko zote, nanyi hamtavikufuru vitu vitakatifu vya Waisraeli na kufa.” Mwenyezi-Mungu aliendelea kuwaambia Mose na Aroni, “Haya ni masharti ya sheria ambayo mimi Mwenyezi-Mungu ninatoa. Waambieni Waisraeli wawaletee ng'ombe jike mwekundu asiye na dosari wala kasoro yoyote, na ambaye hajapata kufungwa nira. Nyinyi mtampa kuhani Eleazari ng'ombe huyo. Atatolewa nje ya kambi na kuchinjwa mbele ya kuhani huyo. “Kisha kuhani Eleazari atachukua kiasi cha damu na kuinyunyiza kwa kidole mara saba, kuelekea upande wa mbele wa hema la mkutano. Ngombe huyo mzima atateketezwa kwa moto mbele ya kuhani. Kila kitu chake kitateketezwa; ngozi, nyama, damu na utumbo wake. Halafu kuhani atachukua mti wa mwerezi, husopo na sufu nyekundu na kuvitia katika moto huo. Baada ya hayo, kuhani atazifua nguo zake na kuoga mwili kwa maji, halafu anaweza kuingia kambini; atakuwa najisi hadi jioni. Mtu atakayemteketeza ng'ombe huyo pia atazifua nguo zake kwa maji na kuoga mwili kwa maji, lakini naye pia atakuwa najisi hadi jioni. Mtu aliye safi atayazoa majivu ya ng'ombe huyo na kuyapeleka mahali safi nje ya kambi. Yatahifadhiwa na kutumiwa na jumuiya nzima ya Israeli kutengeneza maji ya kuondoa najisi, ili kuondoa dhambi. Mtu atakayeyazoa majivu ya ng'ombe huyo lazima azifue nguo zake, lakini atakuwa najisi hadi jioni. Sharti hili ni la kudumu, na litawahusu Waisraeli na watu wengine watakaoishi pamoja nao. “Mtu akigusa maiti ya mtu yeyote, atakuwa najisi kwa siku saba. Siku ya tatu na ya saba mtu huyo atajiosha kwa yale maji ya utakaso, naye atakuwa safi. Lakini akiacha kujitakasa katika siku ya tatu na ya saba, mtu huyo atabaki kuwa najisi. Agusaye maiti, yaani mwili wa mtu aliyekufa, asipojitakasa, analitia najisi hema la Mwenyezi-Mungu, naye atatengwa na wana wa Israeli. Mtu huyo atabaki najisi kwa sababu hakunyunyiziwa yale maji ya utakaso. “Na hii ndiyo sheria ya kufuatwa kama mtu akifia hemani: Kila mtu atakayeingia ndani ya hema hilo, au aliye ndani ya hema hilo, atakuwa najisi kwa siku saba. Kila chombo kilicho wazi ambacho hakina kifuniko juu yake kitakuwa najisi. Mtu yeyote akigusa mwili wa mtu aliyeuawa au aliyekufa kifo cha kawaida nje ya nyumba, au akigusa mfupa wa mtu au kaburi, atakuwa najisi kwa siku saba. “Kwa ajili ya wale waliojitia najisi watachukua majivu ya sadaka ya kuondoa dhambi iliyoteketezwa, majivu hayo yatachanganywa na maji ya mtoni katika chungu. Mtu aliye safi atachukua husopo, halafu ataichovya katika maji hayo, kisha atainyunyizia hema, vyombo vyote vilivyomo ndani ya hema na watu waliokuwamo ndani. Atamnyunyizia pia mtu aliyegusa mfupa wa mtu, au mwili wa mtu aliyeuawa au aliyekufa kifo cha kawaida, au aliyegusa kaburi. Katika siku ya tatu na ya saba, mtu aliye safi atamnyunyizia mtu aliye najisi maji hayo; hivyo katika siku ya saba, atamtakasa mtu huyo aliye najisi, naye atazifua nguo zake na kuoga, na jioni atakuwa safi. “Lakini mtu akiwa najisi asipojitakasa, mtu huyo atakataliwa mbali na jumuiya, kwa kuwa analitia najisi hema la Mwenyezi-Mungu. Kwa vile hakunyunyiziwa maji ya utakaso, yu unajisi. Watu watalishika sharti hili daima. Mtu atakayenyunyiza maji ya kutakasia ataosha nguo zake; naye anayegusa maji hayo ya najisi atakuwa najisi hadi jioni. Chochote atakachogusa mtu najisi kitakuwa najisi, na yeyote atakayekigusa kitu hicho atakuwa najisi mpaka jioni.” Jumuiya nzima ya Waisraeli ilifika katika jangwa la Sinai mnamo mwezi wa kwanza, wakapiga kambi yao huko Kadeshi. Wakiwa huko, Miriamu alifariki, akazikwa. Mahali hapo walipopiga kambi hapakuwa na maji. Kwa hiyo watu jumuiya yote, wakakusanyika kinyume cha Mose na Aroni. Waliwalalamikia wote wakisema, “Afadhali tungekufa pamoja na ndugu zetu mbele ya hema la Mwenyezi-Mungu! Kwa nini mlituleta sisi jumuiya ya Mwenyezi-Mungu huku jangwani? Je, mlituleta ili tufe pamoja na mifugo yetu? Na, kwa nini mlitutoa Misri na kutuleta mahali hapa pabaya hivi? Hapa si mahali pa nafaka, tini, zabibu wala makomamanga. Hata maji ya kunywa hakuna!” Hapo, Mose na Aroni waliondoka kwenye umati wa watu, wakaenda kusimama kwenye mlango wa hema la mkutano, wakasujudu. Basi, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukawatokea, naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Twaa ile fimbo yako, kisha wewe na Aroni ndugu yako, muikusanye jumuiya yote ya watu. Halafu, mbele ya macho yao, uuambie mwamba ulio mbele ya macho yao utoe maji yake. Naam, utaufanya mwamba utoe maji, ili jumuiya nzima ya watu na mifugo yao waweze kunywa.” Mose akaenda kuichukua ile fimbo mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyoamriwa. Kisha Mose na Aroni wakaikusanya jumuiya yote ya watu mbele ya mwamba, naye Mose akawaambia, “Sikilizeni sasa, enyi waasi: Je, tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?” Kisha Mose akainua mkono wake, akaupiga ule mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika kwa wingi, watu wakanywa pamoja na mifugo yao. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Kwa kuwa nyinyi hamkuniamini mimi, wala kunistahi mbele ya macho ya Waisraeli, basi kwa sababu hiyo hamtaiingiza jumuiya hii katika ile nchi niliyowapa.” Hayo ni maji ya Meriba, mahali ambapo Waisraeli walimnungunikia Mwenyezi-Mungu, naye alijionesha kwa utakatifu kati yao. Mose alipeleka wajumbe kutoka Kadeshi kwa mfalme wa Edomu akamwambia: “Ndugu yako, Israeli, asema hivi: Wewe wazijua taabu zote tulizozipata. Jinsi babu zetu walivyokwenda Misri, ambako tuliishi kwa muda mrefu na jinsi Wamisri walivyowatesa babu zetu, wakatutesa na sisi pia. Tulimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akakisikia kilio chetu, akatuletea malaika aliyetuondoa Misri. Sasa tuko hapa Kadeshi, mji unaopakana na nchi yako. Tafadhali uturuhusu tupite nchini mwako. Hatutakanyaga mashamba yenu, wala yale ya mizabibu; wala hatutakunywa maji ya visima vyenu. Tutaifuata barabara kuu ya mfalme na kwenda moja kwa moja bila kugeuka kulia au kushoto, mpaka tutakapotoka katika nchi yako.” Lakini mfalme wa Edomu akamjibu, “La! Hutapita katika nchi yangu, kama ukipita nitatoka na kukushambulia kwa upanga.” Waisraeli wakamwambia, “Sisi tutafuata njia kuu; kama sisi na mifugo yetu tukinywa maji yenu, tutalipa. Tunachoomba tafadhali turuhusu tu, tupite kwa miguu wala hatutaki neno lolote lingine.” Lakini mfalme wa Edomu akasisitiza: “Hatutawaruhusu.” Mara, Waedomu wenye nguvu wakatoka kupigana nao. Basi, Waedomu wakakataa kuwapa ruhusa Waisraeli kupita katika mipaka yao. Waisraeli wakageuka na kushika njia nyingine. Waisraeli wote walisafiri kutoka Kadeshi, wakafika kwenye Mlima Hori. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni huko kwenye Mlima Hori, mpakani mwa nchi ya Edomu, “Aroni atakufa; hataingia katika nchi ambayo nimewapa watu wa Israeli kwa sababu nyinyi wawili mliiasi amri yangu kule Meriba Mchukue Aroni na Eleazari mwanawe, uwalete juu ya Mlima Hori. Kisha, mvue Aroni mavazi yake rasmi, umvalishe mwanawe Eleazari. Aroni atakufa akiwa huko mlimani.” Mose alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Wote watatu walipanda mlimani mbele ya jumuiya yote ya watu. Kisha Mose alimvua Aroni mavazi yake rasmi, akamvalisha mwanawe, Eleazari. Naye Aroni akafa palepale mlimani. Kisha Mose na Eleazari wakateremka chini. Jumuiya yote ya watu ilipopata habari kwamba Aroni amefariki, ikafanya matanga ya siku thelathini. Mfalme mmoja Mkanaani wa Aradi aliyeishi huko Negebu alipopata habari kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, alikwenda kuwashambulia, akawateka baadhi yao. Hapo, Waisraeli wakamwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri wakisema: “Kama utawatia watu hawa mikononi mwetu, basi tutaiangamiza kabisa miji yao.” Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi lao, akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Waisraeli wakawaangamiza kabisa Wakanaani pamoja na miji yao. Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Horma. Waisraeli walifunga safari kutoka Mlima Hori wakapitia njia inayoelekea bahari ya Shamu ili waizunguke nchi ya Edomu. Lakini njiani watu walikufa moyo. Basi, wakaanza kumnungunikia Mungu na Mose, wakisema, “Kwa nini mmetutoa Misri tuje tukafie humu jangwani? Humu hamna chakula wala maji; nasi tumechoshwa na chakula hiki duni.” Hapo Mwenyezi-Mungu akapeleka nyoka wenye sumu miongoni mwa watu, wakawauma hata Waisraeli wengi wakafa. Basi, watu wakamwendea Mose, wakamwambia, “Tumetenda dhambi kwa kumnungunikia Mwenyezi-Mungu na wewe pia. Mwombe Mwenyezi-Mungu atuondolee nyoka hawa.” Kwa hiyo, Mose akawaombea watu. Ndipo Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona.” Basi, Mose akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu aliyeumwa na nyoka alipomtazama nyoka huyo wa shaba, alipona. Waisraeli waliendelea na safari yao, wakapiga kambi huko Obothi. Kutoka huko walisafiri mpaka Iye-abarimu, katika jangwa upande wa mashariki, mwa Moabu. Kutoka huko walisafiri wakapiga kambi yao katika bonde la Zeredi. Kutoka huko walisafiri, wakapiga kambi kaskazini ya mto Arnoni, ambao hutiririka kutoka katika nchi ya Waamori na kupitia jangwani. Mto Arnoni ulikuwa mpaka kati ya Wamoabu na Waamori. Kwa sababu hiyo, imeandikwa katika kitabu cha vita vya Mwenyezi-Mungu: “Mji wa Wahebu nchini Sufa, na mabonde ya Arnoni, na mteremko wa mabonde unaofika hadi mji wa Ari, na kuelekea mpakani mwa Moabu!” Kutoka huko Waisraeli walisafiri mpaka Beeri; yaani kisima ambapo Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Wakusanyeni watu pamoja, nami nitawapa maji.” Hapo Waisraeli waliimba wimbo huu: “Bubujika maji ee kisima! — Kiimbieni! Kisima kilichochimbwa na wakuu kilichochimbwa sana na wenye cheo, kwa fimbo zao za enzi na bakora.” Kutoka jangwani walisafiri mpaka Matana, kutoka Matana mpaka Nahalieli, kutoka Nahalieli mpaka Bamothi, na kutoka Bamothi mpaka kwenye bonde linaloingia nchi ya Moabu, kwenye kilele cha Mlima Pisga, kielekeacho chini jangwani. Waisraeli walimpelekea mfalme Sihoni wa Waamori, ujumbe huu: “Turuhusu tupite katika nchi yako; hatutakwenda pembeni na kuingia mashambani au katika mashamba ya mizabibu, wala hatutakunywa maji ya visima vyenu; tutapita moja kwa moja katika barabara kuu ya mfalme mpaka tumeondoka nchini mwako.” Lakini Sihoni hakuwaruhusu watu wa Israeli wapite katika nchi yake. Aliwakusanya watu wake, akaenda Yahasa Jangwani kuwashambulia Waisraeli. Lakini Waisraeli walimuua, wakaitwaa nchi yake tangu mto Arnoni hadi mto Yaboki, yaani hadi mpaka wa nchi ya Waamoni ambao ulikuwa unalindwa sana. Waisraeli waliiteka miji hii yote nao wakaishi katika miji ya Waamori katika Heshboni na vitongoji vyake. Heshboni ulikuwa mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye hapo awali alikuwa amepigana na mfalme wa Moabu na kuiteka nchi yake yote mpaka mto Arnoni. Ndiyo maana washairi wetu huimba: “Njoni Heshboni na kujenga. Mji wa Sihoni na ujengwe na kuimarishwa. Maana moto ulitoka Heshboni, miali ya moto ilitoka mjini kwa Sihoni, uliuteketeza mji wa Ari wa Moabu, ukaiangamiza milima ya mto Arnoni. Ole wenu watu wa Moabu! Mmeangamizwa, enyi watu wa mungu Kemoshi! Umewafanya watoto wenu wa kiume kuwa wakimbizi, binti zako umewaacha wachukuliwe mateka mpaka kwa Sihoni, mfalme wa Amori. Lakini sasa wazawa wao wameangamizwa, kutoka Heshboni mpaka Diboni, kutoka Nashimu mpaka Nofa, karibu na Medeba.” Basi, Waisraeli wakakaa katika nchi ya Waamori. Kisha Mose alituma watu wapeleleze mji wa Yazeri; wakauteka pamoja na vitongoji vyake, wakawafukuza Waamori waliokaa humo. Waisraeli waligeuka wakafuata njia iendayo Bashani. Mfalme Ogu wa Bashani akatoka na jeshi lake kuwashambulia huko Edrei. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Usimwogope, maana nimemtia mikononi mwako pamoja na watu wake wote na nchi yake yote. Utamtendea kama ulivyomtendea Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekuwa anakaa Heshboni.” Basi, Waisraeli wakamuua Ogu, wanawe na watu wake wote, bila kumwacha hata mtu mmoja, kisha wakaitwaa nchi yake. Waisraeli walianza safari tena, wakaenda kupiga kambi yao katika tambarare za Moabu, mashariki ya mto Yordani, kuelekea mji wa Yeriko. Mfalme Balaki mwana wa Sipori, alijua mambo yote Waisraeli waliyowatendea Waamori. Yeye pamoja na Wamoabu wakashikwa na hofu kubwa juu ya Waisraeli. Waliwaogopa hasa kwa sababu ya wingi wao. Basi Wamoabu wakawaambia viongozi wa Midiani, “Umati huu punde si punde utaharibu kila kitu kandokando yetu kama fahali alavyo majani shambani.” Kwa hiyo, Balaki mwana wa Sipori, aliyekuwa mfalme wa Moabu wakati huo, akapeleka ujumbe kwa Balaamu, mwana wa Beori, huko Pethori, karibu na mto Eufrate, nchini Amawi. Alimwambia Balaamu hivi: “Kuna taifa ambalo limetoka Misri, nalo limeenea kila mahali nchini, tena linatishia kuchukua ardhi yangu. Njoo sasa uwalaani watu hawa kwa ajili yangu maana wana nguvu kuliko mimi. Labda nitaweza kuwashinda na kuwafukuza wasiingie katika nchi yangu, kwa maana najua kuwa wewe ukimbariki mtu hubarikiwa, ukimlaani mtu hulaaniwa.” Basi, maofisa wa Moabu na Midiani wakachukua ada ya mwaguzi, wakaondoka kwenda kwa Balaamu. Walipowasili, walimpa Balaamu ujumbe wa Balaki. Balaamu akawaambia, “Laleni huku usiku huu, nami nitawajulisheni atakayoniambia Mwenyezi-Mungu.” Basi, wazee hao wa Moabu wakakaa na Balaamu. Kisha Mungu alimjia Balaamu, akamwuliza, “Ni nani hawa wanaokaa nawe?” Balaamu akamjibu Mungu, “Balaki mwana wa Sipori amenipelekea ujumbe kwamba kuna watu wa taifa fulani waliotoka Misri, nao wameenea kila mahali nchini. Ameniomba niende kuwalaani watu hao ili pengine afaulu kupigana nao na kuwafukuza.” Mungu akamwambia Balaamu, “Usiende pamoja na watu hawa, wala usiwalaani watu hao maana wamebarikiwa.” Basi, asubuhi yake Balaamu aliamka, akawaambia maofisa wa Balaki, “Rudini nchini mwenu, kwa maana Mwenyezi-Mungu hapendi kuniruhusu kwenda pamoja nanyi.” Kwa hiyo maofisa wa Moabu wakaondoka, wakarudi kwa Balaki, wakamwambia, “Balaamu amekataa kuja pamoja nasi.” Kisha, Balaki akatuma maofisa wengine, wengi zaidi na wa vyeo vya juu kuliko wale wa kwanza. Hao walifika kwa Balaamu, wakamwambia, “Balaki mwana wa Sipori asema hivi: ‘Usikubali kuzuiwa na chochote hata uache kuja kwangu. Nitakutunukia heshima kubwa, na chochote utakachoniomba nitakutimizia. Njoo uwalaani watu hawa.’” Lakini Balaamu akawajibu watumishi wa Balaki, “Hata kama Balaki atanipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, mimi sitaweza kuvunja amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kuhusu jambo lolote, dogo au kubwa. Lakini tafadhalini laleni hapa usiku huu kama wale wenzenu, nami nipate kujua atakachoniambia Mwenyezi-Mungu tena.” Basi, Mungu akamjia Balaamu usiku huo, akamwambia, “Kama watu hawa wamekuja kukuita, nenda pamoja nao, lakini fanya tu kile nitakachokuambia.” Balaamu akaamka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na hao maofisa. Hasira ya Mungu iliwaka kwa sababu Balaamu alikuwa anakwenda; hivyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akakabiliana naye njiani. Wakati huo Balaamu alikuwa amepanda punda wake akiwa na watumishi wake. Basi, punda alimwona malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Kwa hiyo aliiacha njia, akaenda pembeni. Balaamu akampiga huyo punda, akamrudisha njiani. Kisha malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu akatangulia mbele, akasimama mahali penye njia nyembamba, kati ya mashamba ya mizabibu na kuta pande zote mbili. Punda alipomwona malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu, akajisukumiza ukutani na kuubana mguu wa Balaamu hapo. Kwa hiyo Balaamu akampiga tena huyo punda. Kisha malaika akatangulia tena, akasimama mahali pembamba pasipo na nafasi ya kupita kulia wala kushoto. Punda alipomwona huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, akalala chini. Balaamu akawaka hasira, akampiga kwa fimbo yake. Hapo Mwenyezi-Mungu akakifunua kinywa cha huyo punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini hata ukanipiga mara hizi tatu?” Balaamu akamwambia punda, “Wewe umenidhihaki! Kama ningekuwa na upanga ningalikuulia mbali sasa hivi!” Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si yuleyule punda wako aliyekubeba maisha yako yote hadi siku hii ya leo? Je, nimewahi kukutendea namna hii?” Balaamu akajibu, “La.” Hapo, Mwenyezi-Mungu akayafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Balaamu akajitupa chini kifudifudi. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Mbona umempiga punda wako mara hizi tatu? Nimekuja kukuzuia, kwa sababu njia yako ni mbaya. Punda wako ameniona akaniepa mara hizi tatu. Kama asingaligeuka mbali nami hakika ningalikuua wewe na kumwacha hai punda huyu.” Balaamu akamwambia malaika wa Mwenyezi-Mungu “Nimetenda dhambi maana sikujua kwamba umesimama njiani kunizuia. Sasa, kama haikupendezi niendelee na safari hii, basi nitarudi nyumbani.” Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Nenda na watu hawa, lakini utasema tu kile nitakachokuambia.” Basi, Balaamu akaendelea na safari pamoja na viongozi wa Balaki. Balaki alipopata habari kwamba Balaamu anakuja, alitoka kwenda kumlaki mjini Ari, mji uliokuwa ukingoni mwa mto Arnoni kwenye mpaka wa Moabu. Balaki akamwambia Balaamu, “Kwa nini hukuja kwangu mara moja nilipokuita? Je, ulifikiri sitaweza kukutunukia heshima ya kutosha?” Balaamu akamjibu Balaki, “Sasa nimekuja! Lakini, je, nina mamlaka ya kusema chochote tu? Jambo atakaloniambia Mungu ndilo ninalopaswa kusema.” Basi, Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika mjini Kiriath-husothi. Huko Balaki alitoa kafara ya ng'ombe na kondoo, akawagawia nyama Balaamu na maofisa waliokuwa pamoja naye. Kesho yake, Balaki alimchukua Balaamu, akapanda naye mpaka Bamoth-baali; kutoka huko, Balaamu aliweza kuwaona baadhi ya Waisraeli. Balaamu akamwambia Balaki, “Nijengee madhabahu saba hapa kisha uniletee fahali saba na kondoo madume saba.” Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema. Basi, wakatoa juu ya kila madhabahu kafara fahali mmoja na kondoo dume mmoja. Halafu Balaamu akamwambia Balaki, “Baki hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami niende. Labda Mwenyezi-Mungu atakutana nami. Chochote atakachonionesha nitakuja kukuambia.” Basi, Balaamu akaenda peke yake juu ya kilele cha mlima. Mungu akakutana naye. Balaamu akamwambia, “Nimetayarisha madhabahu saba na kutoa kafara fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.” Mwenyezi-Mungu akampa Balaamu maneno atakayosema na kumwambia arudi kwa Balaki. Balaamu akarudi, akamkuta Balaki amesimama palepale karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, pamoja na maofisa wote wa Moabu. Balaamu akamtolea Balaki kauli yake, akasema, “Balaki amenileta hapa kutoka Aramu, naam, mfalme wa Moabu amenileta kutoka milima ya mashariki. ‘Njoo uwalaani watu wa Yakobo kwa ajili yangu, naam, njoo uwalaumu Waisraeli!’ Nitamlaanije mtu ambaye Mungu hakumlaani? Nitawalaumuje watu ambao Mwenyezi-Mungu hakuwalaumu? Kutoka vilele vya majabali nawaona; kutoka juu ya milima nawachungulia. Hilo taifa likaalo peke yake, lisilojiona kuwa sawa na mataifa mengine. Nani awezaye kuwahesabu wingi wa watu wa Yakobo, au kukisia umati wa Waisraeli? Nife kifo cha waadilifu, mwisho wangu na uwe kama wao.” Hapo, Balaki akamwambia Balaamu, “Umenifanyia nini? Nimekuleta hapa uwalaani adui zangu, lakini badala yake umewabariki!” Balaamu akamwambia Balaki, “Sina budi kusema maneno aliyonipa Mwenyezi-Mungu.” Baadaye, Balaki akamwambia Balaamu, “Twende mahali pengine ambapo utaweza kuwaona; hata hivyo utaona tu sehemu yao, hutaweza kuwaona wote. Kisha uwalaani kutoka huko kwa niaba yangu.” Basi, Balaki akamchukua Balaamu kwenye shamba la Sofimu, juu ya kilele cha Mlima Pisga. Hapo akajenga madhabahu saba na kutoa juu ya kila madhabahu kafara ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja. Balaamu akamwambia Balaki, “Baki hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami niende kule ngambo kukutana na Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu akakutana na Balaamu, akampa maneno atakayosema, na kumwambia arudi kwa Balaki. Basi, Balaamu akarudi, akamkuta Balaki amesimama karibu na sadaka ya kuteketezwa pamoja na maofisa wote wa Moabu. Balaki akamwuliza, “Mwenyezi-Mungu amekuambia nini?” Hapo, Balaamu akamtolea Balaki kauli yake: “Inuka, Balaki, usikie, nisikilize ewe mwana wa Sipori. Mungu si mtu, aseme uongo, wala si binadamu, abadili nia yake! Je, ataahidi kitu na asikifanye, au kusema kitu asikitimize? Tazama, nimepewa amri ya kubariki, naye amebariki wala siwezi kuitangua. Mwenyezi-Mungu hajaona ubaya kwa wana wa Yakobo, wala udhia kwa hao wana wa Israeli. Mwenyezi-Mungu Mungu wao yuko pamoja nao, Yeye husifiwa kwa vifijo miongoni mwao, yeye huzipokea sifa zao za kifalme. Mungu aliyewachukua kutoka Misri, huwapigania kwa nguvu kama za nyati. Hakika ulozi hauwezi kuwapinga watu wa Yakobo, wala uchawi dhidi ya watu wa Israeli. Sasa kuhusu Israeli, watu watasema, ‘Tazameni maajabu aliyotenda Mungu!’ Tazama! Waisraeli wameinuka kama simba jike, wanasimama kama simba dume. Ni kama simba asiyelala mpaka amalize mawindo yake, na kunywa damu ya mawindo.” Ndipo Balaki akamwambia Balaamu, “Basi, usiwalaani wala usiwabariki kabisa!” Lakini Balaamu akamjibu Balaki, “Je, sikukuambia kwamba anachosema Mwenyezi-Mungu ndicho ninachopaswa kufanya?” Balaki akamwambia Balaamu, “Njoo; nitakupeleka mahali pengine. Labda Mungu atakubali uwalaani watu hao kutoka huko kwa ajili yangu.” Basi, Balaki akamchukua Balaamu mpaka kwenye kilele cha Mlima Peori, ambapo mtu akisimama anaona jangwani. Balaamu akamwambia Balaki, “Nijengee madhabahu saba hapa, unitayarishie fahali saba na kondoo madume saba.” Balaki akafanya kama alivyoambiwa na Balaamu, kisha akatoa juu ya kila madhabahu kafara fahali mmoja na kondoo dume mmoja. Sasa Balaamu alitambua kwamba Mwenyezi-Mungu alipenda kuwabariki Waisraeli, kwa hiyo hakwenda kupiga bao tena, akawa anaangalia jangwani. Alitazama juu akawaona Waisraeli wamepiga kambi, kila kabila mahali pake. Kisha roho ya Mungu ikamjia, naye akatamka kauli hii ya kinabii: Kauli yangu mimi Balaamu mwana wa Peori kauli ya mtu aliyefumbuliwa macho; kauli ya mtu aliyesikia maneno ya Mungu mtu aliyeona maono ya Mungu Mwenye Nguvu, mtu anayesujudu na kuona wazi. Hema zako zapendeza namna gani enyi watu wa Yakobo; naam, kambi zenu enyi watu wa Israeli! Ni kama mabonde yanayotiririka maji, kama bustani kandokando ya mto, kama mishubiri aliyopanda Mwenyezi-Mungu, kama mierezi kandokando ya maji. Watakuwa na hazina ya kutosha ya maji, mbegu yao itapata maji mengi, mfalme wao atakuwa mkuu kuliko Agagi, na ufalme wake utatukuka sana. Mungu aliwachukua kutoka Misri, naye huwapigania kwa nguvu kama nyati. Atayateketeza mataifa yaliyo adui zao, atavunjavunja mifupa yao, atawachoma kwa mishale yake. Ataotea na kulala chini kama simba, nani atathubutu kumwamsha? Abarikiwe yeyote atakayewabariki nyinyi Waisraeli, alaaniwe yeyote atakayewalaani. Balaki akawaka hasira dhidi ya Balaamu, akakunja mikono kwa ghadhabu na kumwambia, “Nilikuita uwalaani adui zangu, lakini mara hizi zote tatu umewabariki! Sasa! Nenda zako. Nilikuwa nimekuahidi kukupa zawadi nyingi, lakini Mwenyezi-Mungu hakukujalia kupata zawadi hizo, amekunyima!” Balaamu akamjibu Balaki, “Je, sikuwaambia wajumbe uliowatuma kwangu kwamba hata kama ungenipa nyumba yako imejaa fedha na dhahabu, mimi sitaweza kukiuka agizo la Mwenyezi-Mungu, kwa kufanya jambo lolote, jema au baya kwa hiari yangu mwenyewe? Nilisema, atakachosema Mwenyezi-Mungu ndicho nitakachokisema. “Sasa ninarudi kwa watu wangu, lakini kabla sijaondoka, acha nikuambie mambo ambayo watu hao watawatendea watu wako siku zijazo.” Basi, Balaamu akatamka kauli hii: “Kauli yangu mimi Balaamu mwana wa Beori, kauli ya mtu aliyefumbuliwa macho, kauli ya mtu aliyesikia maneno ya Mungu, na mtu ajuaye maarifa ya Mungu Mkuu, mtu aonaye maono ya Mungu Mwenye Nguvu, mtu anayesujudu, macho wazi. Ninamwona, atakayekuja, lakini baadaye, namwona, lakini hayuko karibu. Nyota itatokea kwa wazawa wa Yakobo, atatokea mfalme miongoni mwa Waisraeli. Kwa fimbo yake atawachapa viongozi wa Wamoabu atawaangamiza wazawa wote wa Sethi. Edomu itamilikiwa naye, Seiri itakuwa mali yake, Israeli itapata ushindi mkubwa. Mmoja wa wazawa wa Yakobo atatawala naye atawaangamiza watakaonusurika wa Ari.” Kisha Balaamu akawaangalia Waamaleki, akatoa kauli hii: “Amaleki ni taifa lenye nguvu kuliko yote, lakini mwishoni litaangamia kabisa.” Kisha Balaamu akawaangalia Wakeni, akatoa kauli hii: “Makao yenu ni salama, enyi Wakeni, kama kiota juu kabisa mwambani. Lakini mtateketezwa, enyi Wakeni. Mtachukuliwa mateka na Ashuru mpaka lini?” Tena Balaamu akatoa kauli hii: “Lo! Nani ataishi, Mungu atakapofanya hayo? Meli zitafika kutoka Kitimu, wataishambulia Ashuru na Eberi, lakini nao pia wataangamia milele.” Basi, Balaamu akaondoka, akarudi nyumbani; Balaki pia akaenda zake. Waisraeli walipokuwa huko Shitimu, wanaume walianza kuzini na wanawake wa Moabu. Wanawake hao waliwaalika Waisraeli washiriki matambiko waliyotambikia miungu yao, nao Waisraeli wakala chakula na kuiabudu miungu yao. Ndivyo Waisraeli walivyojiunga na mungu Baali wa Peori, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi yao. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Wachukue viongozi wote wa Israeli, uwanyonge mbele yangu juani, ili ghadhabu yangu dhidi yenu ipite.” Mose akawaambia waamuzi wa Israeli, “Kila mmoja wenu amuue mtu yeyote miongoni mwenu ambaye amejiunga na mungu Baali wa Peori.” Wakati huohuo mtu mmoja akamleta mwanamke mmoja Mmidiani nyumbani kwake, Mose na jumuiya yote ya watu wa Israeli wakiwa wanaomboleza penye lango la hema la mkutano. Basi, Finehasi mwana wa Eleazari mwana wa kuhani Aroni alipoona hayo, aliinuka akatoka katika hiyo jumuiya, akachukua mkuki na kumfuatia yule Mwisraeli mpaka hemani, akawachoma mkuki wote wawili tumboni. Maradhi mabaya yaliyokuwa yamewaangamiza Waisraeli yakakomeshwa. Waliokufa kutokana na maradhi yale mabaya walikuwa watu 24,000. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Aroni, ameizuia hasira yangu dhidi ya Waisraeli; miongoni mwenu ni yeye tu aliyeona wivu kama nilio nao mimi. Ndio maana sikuwaangamiza Waisraeli wote kwa hasira yangu. Kwa hiyo mwambie kwamba ninafanya naye agano la amani. Naagana naye kwamba yeye na wazawa wake watakuwa makuhani milele kwa sababu aliona wivu kwa ajili yangu, Mungu wake, akawafanyia upatanisho Waisraeli.” Huyo Mwisraeli aliyeuawa pamoja na mwanamke wa Kimidiani aliitwa Zimri mwana wa Salu, kiongozi wa jamaa mojawapo katika kabila la Simeoni. Na huyo mwanamke Mmidiani aliyeuawa aliitwa Kozbi binti Suri, aliyekuwa kiongozi wa ukoo fulani huko Midiani. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Wachokoze Wamidiani na kuwaangamiza, kwa sababu waliwachokoza nyinyi kwa hila zao, wakawadanganya kuhusu jambo la Peori, na kwa sababu ya Kozbi, binti yao, aliyeuawa wakati maradhi mabaya yalipozuka kule Peori.” Baada ya yale maradhi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Eleazari mwana wa kuhani Aroni, “Hesabuni jumuiya yote ya Waisraeli, kila mtu kufuatana na jamaa yake. Wahesabuni watu wote wenye umri wa miaka ishirini na zaidi wanaofaa kwenda jeshini.” Mose na kuhani Eleazari wakazungumza na watu kwenye nchi tambarare za Moabu, ngambo ya mto Yordani, karibu na Yeriko, wakawaambia, “Hesabuni watu kuanzia na wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.” Idadi ya Waisraeli waliotoka Misri ni hii: Kwanza ni kabila la Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo. Henoki, Palu, Hesroni na Karmi. Hizo ndizo koo za kabila la Reubeni. Idadi ya wanaume waliohesabiwa ni 43,730. Wazawa wa Palu walikuwa Eliabu, na wanawe Nemueli, Dathani na Abiramu. (Hawa wawili: Dathani na Abiramu, ndio waliokuwa wamechaguliwa miongoni mwa jumuiya, lakini wakampinga Mose na Aroni, na kujiunga na wafuasi wa Kora wakati walipomwasi Mwenyezi-Mungu. Wakati huo ardhi ilifunguka ikawameza, wakafa pamoja na Kora na wafuasi wake moto ulipoangamiza watu 250; wakawa onyo kwa watu. Pamoja na hayo wana wa Kora hawakufa.) Kabila la Simeoni. Nemueli, Yamini, Yakini, Zera na Shauli. Hizo ndizo koo za kabila la Simeoni, jumla yao wanaume 22,000. Kabila la Gadi lilikuwa na jamaa za Sefoni, Hagi, Shuni, Ozni, Eri, Arodi na Areli. Hizo ndizo koo za kabila la Gadi, jumla wanaume 40,500. Kabila la Yuda lilikuwa na wanawe wa Yuda Eri na Onani. Hawa walifia nchini Kanaani. Kabila la Yuda lilikuwa na jamaa za Shela, Peresi, na Zera. Kutoka kwa Peresi, familia ya Hesroni na Hamuli. Hizo ndizo koo za Yuda, jumla wanaume 76,500. Kabila la Isakari lilikuwa na jamaa za Tola, Puva, Yashubu na wa Shimroni. Hizo ndizo koo za Isakari, jumla wanaume 64,300. Kabila la Zebuluni lilikuwa na jamaa za Seredi, wa Eloni na wa Yaleeli. Hizo ndizo koo za Zebuluni, jumla wanaume 60,500. Kabila la Yosefu baba yao Manase na Efraimu. Kabila la Manase lilikuwa na jamaa ya: Makiri, Gileadi. Yezeri, Heleki, Asrieli, Shekemu, Shemida na Heferi. Selofehadi, mwana wa Heferi hakupata watoto wa kiume bali wa kike tu, nao ni Mala, Noa, Hogla, Milka na Tirza. Hizo ndizo koo za Manase, jumla wanaume 52,700. Kabila la Efraimu lilikuwa na jamaa za Shuthela, Bekeri na Tahani. Ukoo wa Erani ulikuwa na jamaa ya Shuthela. Hizo ndizo koo za Efraimu, jumla wanaume 32,500. Zote hizo zilitokana na Yosefu. Kabila la Benyamini lilikuwa na jamaa za Bela, Ashbeli, Ahiramu, Shufamu na Hufamu. Koo za Ardi na Naamani, zilitokana na Bela. Hizo ndizo koo za Benyamini, jumla wanaume 45,600. Kabila la Dani lilikuwa na jamaa ya Shuhamu; ukoo ulikuwa na wanaume 64,400. Kabila la Asheri lilikuwa na jamaa za Imna, Ishvi na Beria. Koo za Heberi na Malkieli zilitokana na Beria. Asheri alikuwa na binti aliyeitwa Sera. Hizo ndizo koo za kabila la Asheri, jumla wanaume 53,400. Kabila la Naftali lilikuwa na jamaa za Yaseeli, Guni, Yeseri na Shilemu. Hizi ndizo koo za kabila la Naftali, jumla wanaume 45,400. Idadi ya wanaume Waisraeli waliohesabiwa ilikuwa 601,730. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Makabila haya yatagawiwa nchi iwe urithi wao, kulingana na idadi ya majina yao. Kabila kubwa litapewa sehemu yao kubwa na dogo litapewa sehemu yao ndogo. Kila kabila litapewa urithi wake kulingana na idadi ya watu wake. Hata hivyo ugawaji wa nchi utafanywa kwa kura. Kila kabila litarithi kulingana na majina ya ukoo wao. Urithi wa kila kabila utagawanywa kwa kura, kila kabila litapata kulingana na ukubwa au udogo wake.” Hizi ndizo koo za Walawi zilizoorodheshwa na jamaa zao: Gershoni, Kohathi na Merari, Pamoja na jamaa za Libni, Hebroni, Mahli, Mushi na Kora. Kohathi alikuwa baba yake Amramu. Mkewe Amramu aliitwa Yokebedi binti yake Lawi, aliyezaliwa Misri. Huyu alimzalia Amramu watoto wawili wa kiume, Aroni na Mose, na binti mmoja, Miriamu. Aroni alikuwa na watoto wa kiume wanne: Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari. Nadabu na Abihu walikufa walipomtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya moto usiofaa. Idadi ya Walawi wanaume wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi ilikuwa 23,000. Hawa hawakuhesabiwa pamoja na Waisraeli wengine kwa sababu wao hawakupewa urithi wowote miongoni mwao. Hao ndio wanaume Waisraeli walioorodheshwa na Mose na kuhani Eleazari katika nchi tambarare za Moabu, ngambo ya mto Yordani, karibu na Yeriko. Miongoni mwao hakuwamo hata mtu mmoja aliyesalia kati ya wale waliohesabiwa na Mose na kuhani Aroni ambao walifanya sensa ya kwanza jangwani Sinai. Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema kwamba wote watafia jangwani, na kweli hakuna hata mmoja wao aliyebaki hai, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. Mala, Noa, Hogla, Milka na Tirza walikuwa binti zake Selofehadi. Naye Selofehadi alikuwa mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase mwanawe Yosefu. Basi, hao binti wanne walimwendea Mose, wakasimama mbele yake na kuhani Eleazari na viongozi wote wa jumuiya ya Waisraeli, kwenye mlango wa hema la mkutano, wakasema, “Baba yetu alifia jangwani nyikani na bila mtoto yeyote wa kiume. Yeye hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora waliokusanyika dhidi ya Mwenyezi-Mungu, bali alikufa kutokana na dhambi yake mwenyewe. Kwa nini basi jina la baba yetu lifutwe katika ukoo wake kwa sababu hakuwa na mtoto wa kiume? Tupe urithi pamoja na ndugu zake baba yetu.” Mose akaleta lalamiko lao mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Wanachosema binti za Selofehadi ni kweli; wape urithi pamoja na ndugu za baba yao, wachukue urithi wake. Kisha waambie Waisraeli kwamba mtu yeyote akifa bila kuacha mtoto wa kiume, urithi wake atapewa binti yake. Ikiwa hana binti, basi urithi huo watapewa ndugu zake wa kiume. Na ikiwa hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utawaendea baba zake, wakubwa na wadogo. Na ikiwa baba yake hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utakuwa wa jamaa yake wa karibu, naye ataumiliki kama mali yake. Hii itakuwa kanuni na sheria kwa Waisraeli, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu nilivyokuamuru.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Panda juu ya Mlima huu wa miinuko ya Abarimu uitazame nchi ambayo nimewapa Waisraeli. Ukisha iona, nawe pia utafariki kama ndugu yako Aroni alivyofariki, kwa sababu hamkuitii amri yangu kule jangwani Sini. Wakati jumuiya yote ya watu walipolalamika juu yangu kule Meriba, hamkuacha utukufu wangu uonekane mbele yao walipotaka wapewe maji.” (Meriba ni chemchemi ya maji ya Kadeshi katika jangwa la Sini). Naye Mose akamwomba Mwenyezi-Mungu, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu uliye asili ya uhai wote, nakuomba umteue mtu wa kuisimamia jumuiya hii, ambaye atawatangulia na kuwaongoza katika shughuli zao zote, ili wasije wakawa kama kondoo wasio na mchungaji.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mtwae Yoshua mwana wa Nuni, mtu mwenye roho nzuri, kisha umwekee mikono, na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote, umkabidhi jukumu hilo. Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli imtii. Yeye atamtegemea kuhani Eleazari ambaye atamjulisha matakwa yangu kwa kutumia jiwe la kauli. Kwa njia hii, Eleazari atamwongoza Yoshua na jumuiya yote ya Waisraeli wanapotoka na wanapoingia.” Mose akafanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Alimtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote ya Waisraeli. Kisha akamwekea mikono kichwani na kumpa mamlaka kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waamuru Waisraeli ifuatavyo: Nyinyi mtanitolea kwa wakati wake tambiko zitakiwazo: Vyakula vya kuteketezwa kwa moto, vyenye harufu nzuri ya kupendeza. Waambie kwamba sadaka watakayonitolea ya kuteketezwa kwa moto, itakuwa ifuatavyo: Wanakondoo wawili wa mwaka mmoja wasio na dosari yoyote, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa ya kila siku. Mwanakondoo mmoja atatolewa asubuhi na wa pili jioni; kila mmoja atatolewa pamoja na sadaka ya nafaka ya kilo moja ya unga uliochanganywa pamoja na lita moja ya mafuta bora yaliyopondwa. Hii ni sadaka ya kutolewa kila siku inayoteketezwa kabisa motoni, ambayo ilitolewa kwa mara ya kwanza mlimani Sinai kama sadaka ya chakula, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Sadaka ya kinywaji itakayotolewa na kila mwanakondoo ni lita moja ya divai. Utaimimina sadaka hii ya kinywaji kikali mahali patakatifu. Wakati wa jioni utamtoa yule mwanakondoo mwingine kama sadaka ya nafaka na kama sadaka ya kinywaji utaitoa kama sadaka ya kuteketezwa kwa moto, sadaka yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. “Siku ya Sabato, mtatoa sadaka ya wanakondoo wawili wa kiume wa mwaka mmoja wasio na dosari, sadaka ya nafaka ya kilo mbili za unga laini uliochanganywa na mafuta, na sadaka yake ya kinywaji. Sadaka hii ya kuteketezwa itatolewa kila siku ya Sabato licha ya ile sadaka ya kila siku pamoja na sadaka yake ya kinywaji. “Mwanzoni mwa kila mwezi, mtamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa: Fahali wadogo wawili, kondoo dume mmoja na, wanakondoo saba madume wa mwaka mmoja, wasio na dosari. Mtatoa sadaka ya nafaka ya unga laini kilo tatu, uliochanganywa na mafuta kwa kila fahali mmoja; mtatoa kilo mbili za unga kwa kila kondoo dume, na kilo moja ya unga kwa kila mwanakondoo. Sadaka hizi za kuteketezwa ni sadaka za chakula zenye harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Kipimo cha sadaka ya kinywaji kinachohitajika ni lita 2 za divai kwa kila fahali; lita moja u nusu kwa kila kondoo dume, na lita moja kwa kila mwanakondoo. Hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi katika mwaka mzima. Tena mtamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuondoa dhambi, beberu mmoja, licha ya ile sadaka ya kuteketezwa ya kila siku na sadaka yake ya kinywaji. “Siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza ni Pasaka ya Mwenyezi-Mungu. Siku ya kumi na tano ya mwezi huohuo ni sikukuu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza kutakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo hamtafanya kazi. Mtatoa sadaka ya kuteketezwa kama sadaka ya chakula kwa Mwenyezi-Mungu: Fahali wachanga wawili, kondoo dume mmoja, wanakondoo madume saba wa mwaka mmoja, wote wawe bila dosari. Sadaka ya nafaka itakayoandamana nazo itakuwa ya unga safi uliochanganywa na mafuta, kilo tatu kwa kila fahali, kilo mbili kwa kila kondoo dume, na kilo moja kwa kila mmoja wa wale wanakondoo saba. Mtatoa pia beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi ili kuwafanyia upatanisho. Mtatoa vitu hivi licha ya ile sadaka ya kuteketezwa ya kawaida inayotolewa kila siku asubuhi. Vivyo hivyo, kwa muda wa siku saba, mtatoa sadaka ya kuteketezwa ya kawaida ya chakula kwa kuteketezwa, ambayo ni harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Hii mtaitoa licha ya ile sadaka ya kuteketezwa ya kila siku na sadaka yake ya kinywaji. Katika siku ya saba mtafanya mkutano mtakatifu; msifanye kazi. “Mnamo siku ya kwanza ya sikukuu ya majuma wakati mnapomtolea Mwenyezi-Mungu malimbuko ya nafaka zenu, mtafanya mkutano mtakatifu; msifanye kazi. Mtatoa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu: Fahali wachanga wawili, kondoo dume mmoja, na wanakondoo saba madume wa mwaka mmoja, wote hao wawe hawana dosari. Sadaka ya nafaka itakayoandamana nazo itakuwa ya unga safi uliochanganywa na mafuta kilo tatu kwa kila fahali, kilo mbili kwa kila kondoo dume, na kilo moja kwa kila mwanakondoo. Mtatoa pia beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi ili kuwafanyia upatanisho. Mtatoa vitu hivi licha ya ile sadaka ya kuteketezwa ya kawaida pamoja na sadaka yake ya kinywaji. “Siku ya kwanza ya mwezi wa saba, mtafanya mkutano mtakatifu. Msifanye kazi. Hiyo ni siku ya kupiga tarumbeta. Mtatoa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu: Fahali wachanga wawili, kondoo madume wawili, na wanakondoo wa kiume saba wa mwaka mmoja, wote wawe wasio na dosari yoyote. Mtatoa pia sadaka yake ya nafaka ya unga safi uliochanganywa na mafuta: Kilo tatu kwa kila fahali, kilo mbili kwa kila kondoo dume, na kilo moja kwa kila mwanakondoo. Tena mtatoa beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi ili kuwafanyia upatanisho. Mtatoa vitu hivi licha ya ile sadaka ya kuteketezwa ya mwezi mpya na sadaka yake ya nafaka, na sadaka ya kila siku ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka zake za kinywaji kama inavyotakiwa kuwa harufu nzuri ipendezayo, ni sadaka kwa Mwenyezi-Mungu iliyoteketezwa kwa moto. “Siku ya kumi ya mwezi wa saba mtafanya mkutano mtakatifu. Siku hiyo ni lazima mfunge na msifanye kazi. Mtamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa kwa moto, harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu: Fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja, wanakondoo saba wa mwaka mmoja. Wote wasiwe na dosari. Licha ya vitu hivi mtatoa sadaka ya unga safi uliochanganywa na mafuta kilo tatu pamoja na huyo fahali, kilo mbili pamoja na yule kondoo dume, na kilo moja kwa kila mwanakondoo. Mtatoa pia beberu mmoja kwa sadaka ya kuondoa dhambi licha ya sadaka ya kufanyiwa upatanisho, pamoja na sadaka ya kawaida ya kuteketezwa na sadaka yake ya nafaka na sadaka zake za kinywaji. “Siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, mtafanya mkutano mtakatifu. Hamtafanya kazi siku hiyo. Mtaadhimisha sikukuu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu kwa siku saba. Mtatoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto, iliyo harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi-Mungu: Fahali wachanga kumi na watatu, kondoo madume wawili, wanakondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja. Wote wawe bila dosari. Sadaka itakayoandamana nazo itakuwa unga safi uliochanganywa na mafuta: Kilo tatu kwa kila fahali, kilo mbili kwa kila kondoo, na kilo moja kwa kila mwanakondoo. Mtatoa pia beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi, licha ya ile sadaka ya kawaida ya kuteketezwa, pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji. “Siku ya pili mtatoa: Fahali wachanga kumi na wawili, kondoo madume wawili, wanakondoo wa kiume kumi na wanne, wa mwaka mmoja wasio na dosari. Mtatoa pia sadaka ya nafaka na sadaka za vinywaji pamoja na wale fahali, kondoo na wanakondoo, kulingana na idadi yao. Mtatoa pia beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi, licha ya sadaka ya kuteketezwa ya kawaida pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji. “Siku ya tatu mtatoa: Fahali kumi na mmoja, kondoo wawili, wanakondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja, wasio na dosari. Mtawatolea pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji kama ilivyotakiwa kulingana na idadi yao. Vilevile mtatoa beberu mmoja kwa sadaka ya kuondoa dhambi, licha ya ile sadaka ya kawaida ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji. “Siku ya nne mtatoa: Fahali kumi, kondoo madume wawili, wanakondoo kumi na wanne, wasio na dosari. Mtatoa pia sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji pamoja na hao fahali na kondoo na wanakondoo kulingana na idadi yao, kama inavyotakiwa. Mtatoa pia beberu mmoja kwa sadaka ya kuondoa dhambi licha ya sadaka ya kawaida ya kuteketezwa, pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji. “Siku ya tano, mtatoa fahali tisa, kondoo wawili, wanakondoo madume kumi na wanne wa mwaka mmoja wasio na dosari. Mtatoa pia sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji pamoja na hao fahali na kondoo na wanakondoo kulingana na idadi yao kama inavyotakiwa. Mtatoa pia beberu mmoja kwa sadaka ya kuondoa dhambi, licha ya sadaka ya kawaida ya kuteketezwa, pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji. “Siku ya sita mtatoa fahali wanane, kondoo madume wawili, wanakondoo madume kumi na wanne wa mwaka mmoja wasio na dosari. Mtatoa pia sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji pamoja na hao fahali, kondoo dume na wanakondoo kulingana na idadi yao, kama inavyotakiwa. Mtatoa pia beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi, pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka zake za kinywaji. “Siku ya saba mtatoa fahali saba, kondoo madume watatu, wanakondoo madume kumi na wanne wa mwaka mmoja, wasio na dosari. Mtatoa pia sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji pamoja na hao fahali, kondoo dume, na wanakondoo, kulingana na idadi yao, kama wanavyotakiwa. Mtatoa pia beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi, licha ya ile sadaka ya kawaida ya kuteketezwa, pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji. “Siku ya nane mtakuwa na mkutano mkubwa. Msifanye kazi siku hiyo. Mtatoa sadaka ya kuteketezwa iliyo harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi-Mungu: Fahali mmoja, kondoo dume mmoja, na wanakondoo madume saba wa mwaka mmoja wasio na dosari. Mtatoa pia sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji pamoja na huyo fahali, huyo kondoo dume, na wale wanakondoo kulingana na idadi yao kama inavyotakiwa. Pia mtatoa beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi, licha ya ile sadaka ya kawaida ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka ya kinywaji. “Haya ndiyo maagizo kuhusu sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na sadaka za amani mtakazomtolea Mwenyezi-Mungu wakati wa sikukuu zenu zilizopangwa. Licha ya hizi zote, zipo pia sadaka za kuteketezwa, za nafaka na za kinywaji, ambazo mnamtolea Mwenyezi-Mungu kutimiza nadhiri zenu na sadaka zenu za hiari.” Basi, Mose akawaambia Waisraeli kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru. Kisha Mose alizungumza na viongozi wa makabila ya Israeli, akawaambia, “Hili ndilo neno lililoamriwa na Mwenyezi-Mungu: “Mtu akiweka nadhiri kwa Mwenyezi-Mungu au akiahidi kwa kiapo na kujifunga nafsi yake kwa ahadi, ni lazima atimize ahadi yake; ni lazima atekeleze yote yale aliyotamka kwa kauli yake. “Msichana ambaye bado anaishi nyumbani kwa baba yake akiweka nadhiri kwa Mwenyezi-Mungu na kujifunga mwenyewe kwa ahadi, na baba yake akawa amesikia ahadi hiyo, asimpinge, basi, nadhiri zake alizoweka zitambana na kila ahadi aliyotoa itambana. Lakini kama baba yake akisikia juu ya nadhiri hiyo, akampinga, basi nadhiri zake na ahadi yake havitambana. Mwenyezi-Mungu atamsamehe kwa sababu baba yake amelipinga jambo hilo. “Ikiwa msichana ataolewa baada ya kuweka nadhiri, au kuahidi bila ya kufikiri vizuri kwanza, na akajifunga mwenyewe, halafu mumewe akasikia jambo hilo asimpinge, basi nadhiri zake zitambana na ahadi zake zitambana. Lakini kama mume wake akisikia jambo hilo akampinga, basi huyo mumewe atabatilisha nadhiri ya mkewe na tamko lake alilotoa bila kufikiri; naye Mwenyezi-Mungu atamsamehe. “Lakini nadhiri au ahadi yoyote aliyoiweka mama mjane au mwanamke aliyepewa talaka ambayo kwayo amejifunga, ni lazima imbane. “Mwanamke aliyeolewa akiweka nadhiri au akiahidi kwa kiapo akiwa nyumbani kwa mumewe, kisha mume wake akasikia jambo hilo lakini asimpinge, wala kumwambia kitu, basi, nadhiri zake zote zitambana; kadhalika na ahadi zake zote zitambana. Lakini kama mumewe atakaposikia habari zake, akizitangua na kuzibatilisha, basi, hata kama alitaka kutimiza nadhiri au ahadi zake, hatawajibika kuzitimiza; mumewe atakuwa amezitangua na Mwenyezi-Mungu atamsamehe. Mumewe anaweza kuthibitisha au kutangua nadhiri au ahadi yoyote inayomfunga. Lakini ikiwa mumewe hatasema neno lolote tangu siku atakaposikia habari za nadhiri au ahadi za mkewe, basi atakuwa amezithibitisha siku hiyo alipopata habari zake kwa sababu hakusema chochote. Lakini akizibatilisha na kuzitangua muda fulani baada ya kusikia habari zake, basi yeye atakuwa na lawama kwa kosa la mkewe.” Hizi ndizo kanuni ambazo Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose juu ya mume na mkewe; baba na binti yake, huyo binti akiwa bado kijana na anakaa nyumbani kwa baba yake. Mwenyezi-Mungu aliongea na Mose, akamwambia, “Walipize kisasi Wamidiani mambo waliyowatenda Waisraeli; kisha wewe utafariki.” Basi Mose akazungumza na watu akawaambia, “Watayarisheni watu kwa vita waende kuwashambulia Wamidiani kumlipizia Mwenyezi-Mungu kisasi. Kutoka kila kabila la Israeli, mtapeleka watu 1.000 vitani.” Basi, watu 1,000 walitolewa kutoka kila kabila miongoni mwa maelfu ya Waisraeli, jumla wanaume 12,000 wenye silaha. Mose aliwapeleka vitani chini ya uongozi wa Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akiwa na vyombo vya mahali patakatifu na tarumbeta za kutoa ishara. Waliishambulia nchi ya Midiani, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose, wakawaua wanaume wote. Miongoni mwa watu hao waliouawa, kulikuwako wafalme watano wa Midiani: Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba. Vilevile walimuua Balaamu mwana wa Beori. Waisraeli waliteka nyara: Ng'ombe, kondoo na mali yao yote. Miji yao yote, makazi yao na kambi zao zote waliziteketeza kwa moto. Walichukua nyara zote na mateka yote, ya watu na ya wanyama, wakampelekea Mose na Eleazari, na jumuiya yote ya Waisraeli iliyokuwa kambini katika nchi tambarare za Moabu, ngambo ya Yordani karibu na Yeriko. Mose, kuhani Eleazari, na viongozi wote wa jumuiya ya Waisraeli walitoka kambini, wakaenda kuwalaki wanajeshi. Mose alikasirishwa na maofisa wa jeshi na makamanda waliosimamia makundi ya majeshi 1,000 na makundi ya wanajeshi mamia waliorudi kutoka vitani. Mose akawauliza, “Kwa nini mmewaacha wanawake hawa wote hai? Kumbukeni kwamba wanawake ndio waliofuata shauri la Balaamu, wakasababisha Waisraeli wamwasi Mwenyezi-Mungu kule Peori hata maradhi mabaya yakawajia watu wake Mwenyezi-Mungu. Kwa hiyo basi, waueni watoto wote wa kiume na kila mwanamke aliyewahi kulala na mwanamume. Lakini msiwaue wasichana wote ambao hawajapata kulala na mwanamume; waacheni hai kwa ajili yenu wenyewe. Wote wale walio miongoni mwenu ambao wameua mtu au kugusa maiti ni lazima wakae nje ya kambi kwa muda wa siku saba; jitakaseni pamoja na mateka wenu katika siku ya tatu na ya saba. Ni lazima mtakase pia kila vazi, kila kitu kilichotengenezwa kwa ngozi, kwa manyoya ya kondoo au kwa mti.” Kuhani Eleazari akawaambia wanaume waliorudi vitani, “Hii ndiyo sheria ambayo Mwenyezi-Mungu amempa Mose. Dhahabu, fedha, shaba, chuma, bati na madini ya risasi, yaani vitu vyote ambavyo vinastahimili moto, vitatakaswa kwa kupitishwa motoni. Hata hivyo, ni lazima vitakaswe kwa maji ya utakaso. Vitu vingine vyote ambavyo haviwezi kustahimili moto vitatakaswa kwa maji ya utakaso. Siku ya saba ni lazima muyafue mavazi yenu; ndipo mtakapokuwa safi na kuruhusiwa kuingia kambini.” Mwenyezi-Mungu akaongea na Mose, akamwambia, “Wewe na kuhani Eleazari, pamoja na viongozi wa koo za jumuiya ya Waisraeli, fanyeni hesabu ya nyara ya vitu, watu na wanyama. Gaweni nyara katika mafungu mawili, fungu moja la wanajeshi waliokwenda vitani na fungu lingine kwa ajili ya jumuiya nzima. Kisha kutokana na lile fungu la wanajeshi waliokwenda vitani, tenga zaka kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu: Kitu kimoja kutoka kila vitu 500, iwe ni watu, ng'ombe, punda, kondoo au mbuzi, umpe kuhani Eleazari kuwa sadaka kwa Mwenyezi-Mungu. Kutoka lile fungu la jumuiya nzima, chukua sehemu moja ya kila hamsini, iwe ni watu, ng'ombe, punda, kondoo na mbuzi. Hivyo utawapa Walawi ambao wana wajibu wa kuhudumu katika hema la Mwenyezi-Mungu.” Mose na kuhani Eleazari walifanya kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Nyara walizoteka wanajeshi zilikuwa: Kondoo 675,000, ng'ombe 72,000, punda 61,000, na wasichana ambao hawakuwa wamelala na mwanamume 32,000. Nusu yake, sehemu ambayo iligawiwa wanajeshi waliokwenda vitani, ilikuwa kondoo 337,500, katika hao 675 walitolewa kwa Mwenyezi-Mungu. Ngombe wa wanajeshi walikuwa 36,000, na katika hao 72 walitolewa zaka kwa Mwenyezi-Mungu. Punda wao walikuwa 30,500, na katika hao 61 walitolewa zaka kwa Mwenyezi-Mungu. Watu walikuwa 16,000, na katika hao sehemu ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa ni watu thelathini na wawili. Basi, Mose akampa kuhani Eleazari zaka hiyo iliyotolewa kwa Mwenyezi-Mungu, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Ile nusu waliopewa Waisraeli, ambayo Mose aliitenga na ile nusu waliyopewa wanajeshi waliokwenda vitani, ilikuwa kondoo 337,500, ng'ombe 36,000, punda 30,500, na watu 16,000. Kutoka nusu hii waliyopewa Waisraeli, Mose alitwaa mmoja kati ya kila mateka hamsini na wanyama hamsini, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, akawapa Walawi ambao walihudumu katika hema la Mwenyezi-Mungu. Kisha maofisa wa majeshi, makapteni na makamanda wa askari wakamwendea Mose, wakamwambia “Watumishi wako tumewahesabu askari wote walio chini yetu na tumeona kwamba hakuna hata mmoja wao anayekosekana. Basi, tumeleta vyombo vya dhahabu, vikuku, bangili, pete za mhuri, vipuli na shanga ambavyo kila mtu alipata. Tumevitoa ili nafsi zetu zifanyiwe upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu.” Mose na kuhani Eleazari wakapokea vitu vyote vilivyonakshiwa kwa dhahabu. Jumla ya dhahabu yote waliyomtolea Mwenyezi-Mungu ilikuwa karibu kilo 200. (Kila askari alijichukulia nyara zake binafsi). Basi, Mose na kuhani Eleazari wakaipokea dhahabu hiyo kutoka kwa makamanda wakaipeleka katika hema la mkutano, iwe ukumbusho wa Waisraeli mbele ya Mwenyezi-Mungu. Makabila ya Reubeni na Gadi yalikuwa na mifugo mingi sana. Basi, walipoona kwamba eneo la Yazeri na Gadi lilifaa kwa mifugo, waliwaendea Mose, kuhani Eleazari na viongozi wa jumuiya, wakawaambia, “Miji ya Atarothi, Diboni, Yazeri, Nimra, Heshboni, Eleale, Sebamu, Nebo na Beoni, nchi ambayo Mwenyezi-Mungu alishinda kwa ajili ya jumuiya ya Israeli, ni nchi nzuri kwa mifugo, nasi tunayo mifugo mingi sana. Basi, kama mkitukubalia tunawaomba mtupe nchi hii iwe mali yetu; msituvushe ngambo ya mto Yordani.” Mose akawajibu watu wa makabila ya Gadi na Reubeni, “Je, mnataka kubaki hapa huku ndugu zenu Waisraeli wanakwenda vitani? Mbona mnawavunja moyo Waisraeli wasiende katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu amewapa? Hivyo ndivyo walivyofanya babu zenu nilipowatuma kutoka Kadesh-barnea kuipeleleza nchi. Wao walikwenda hadi bonde la Eshkoli, wakaiona nchi, lakini waliporudi, waliwavunja moyo Waisraeli ili wasiingie katika nchi aliyowapa Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu aliwaka hasira siku hiyo, akaapa akisema, ‘Hakika hakuna mtu yeyote kati ya watu waliotoka Misri mwenye umri wa miaka ishirini na zaidi atakayeiona nchi niliyoapa kuwapa Abrahamu, Isaka na Yakobo, kwa sababu hawakunitii kikamilifu.’ Wote hawataiona, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, maana wao wamenitii kikamilifu. Mwenyezi-Mungu aliwaka hasira dhidi ya Waisraeli, akawafanya watangetange jangwani kwa muda wa miaka arubaini; kizazi kizima kilichokuwa kimefanya maovu mbele yake kikafariki. Na sasa, enyi kizazi cha wenye dhambi, mmezuka mahali pa wazee wenu, kuongeza tena hasira kali ya Mwenyezi-Mungu dhidi ya Waisraeli. Kama nyinyi mkikataa kumfuata, yeye atawaacheni tena jangwani, nanyi mtasababisha watu hawa wote waangamie.” Basi, wakamwendea Mose, wakamwambia, “Kwanza turuhusu tuwajengee kondoo wetu mazizi, na watoto wetu miji hapa. Lakini sisi wenyewe tutachukua silaha zetu tayari kwenda vitani pamoja na ndugu zetu Waisraeli, na tutakuwa mstari wa mbele vitani hadi tuwafikishe mahali watakapokaa. Wakati huo watoto wetu watakaa kwenye miji yenye ngome, ili kujilinda na wenyeji wa nchi hii. Hatutarudi nyumbani hadi hapo Waisraeli wengine wote watakapomiliki maeneo yao waliyogawiwa. Hatutamiliki mali yoyote miongoni mwao ngambo ya mto Yordani, kwa sababu sisi tumepata maeneo yetu ngambo hii, mashariki ya mto Yordani.” Mose akawaambia, “Kama kweli mtafanya kama mlivyosema, basi papa hapa mbele ya Mwenyezi-Mungu, chukueni silaha zenu kwenda vitani. Kila mpiganaji wenu atavuka mto Yordani na mkiwa chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu, mtawashambulia adui zetu mpaka Mwenyezi-Mungu awashinde, na kuimiliki nchi. Mkisha fanya hayo, mtarudi, maana mtakuwa mmetimiza wajibu wenu kwa Mwenyezi-Mungu na ndugu zenu Waisraeli. Kisha Mwenyezi-Mungu atakubali nchi hii ya mashariki ya Yordani kuwa mali yenu. Lakini nawaonyeni kwamba msipotimiza ahadi yenu, mtakuwa mnamtendea Mwenyezi-Mungu dhambi; jueni kwa hakika kwamba mtaadhibiwa. Wajengeeni watoto wenu miji na kondoo wenu mazizi; lakini fanyeni kama mlivyoahidi.” Kisha, watu wa Gadi na wa Reubeni wakamwambia Mose, “Sisi watumishi wako tutafanya kama ulivyotuamuru. Wake zetu, watoto wetu na kondoo na ng'ombe, watabaki hapa katika miji ya Gileadi. Lakini sisi watumishi wako tuko tayari kwenda vitani chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu. Tutavuka mto Yordani na kupigana, kama ulivyosema.” Basi, Mose akatoa amri zifuatazo kwa kuhani Eleazari, kwa Yoshua mwana wa Nuni, na kwa viongozi wa jamaa za makabila ya Waisraeli: “Ikiwa watu wa Gadi na wa Reubeni watavuka mto Yordani pamoja nanyi wakiwa na silaha zao chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu, mkashinda na kuichukua nchi hiyo, basi mtawapa nchi ya Gileadi iwe mali yao. Lakini kama hawatavuka mto Yordani pamoja nanyi na silaha zao, basi watamiliki sehemu ya nchi ya Kanaani pamoja nanyi.” Watu wa Gadi na wa Reubeni wakajibu, “Bwana, sisi tutafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyotuambia sisi watumishi wako. Chini ya uongozi wake Mwenyezi-Mungu, tutavuka na silaha zetu mpaka nchini Kanaani, lakini nchi tuliyopewa hapa mashariki ya Yordani itakuwa mali yetu.” Basi, Mose akawapa watu wa makabila ya Gadi na Reubeni na nusu ya kabila la Manase mwana wa Yosefu, nchi yote ya mfalme Sihoni wa Waamori na nchi ya mfalme Ogu wa Bashani pamoja na miji na maeneo yaliyokuwa kandokando ya miji hiyo. Kabila la Reubeni likaijenga miji ya Diboni, Atarothi, Aroeri, Atroth-shofani, Yazeri, Yogbeha, Beth-nimra na Beth-harani, miji yenye ngome na mazizi ya kondoo. Kabila la Gadi lilijenga miji ya Heshboni, Eleale, Kiriathaimu, Nebo na Baal-meoni (majina ya hiyo miji yalibadilishwa), na Sibma. Miji waliyoijenga waliipa majina mengine. Wazawa wa Makiri, mwana wa Manase, waliishambulia nchi ya Gileadi, wakaiteka na kuwafukuza Waamori waliokuwa wanakaa humo. Kwa hiyo, Mose akawapa watu wa ukoo wa Makiri mwana wa Manase, nchi ya Gileadi, nao wakakaa humo. Yairi, wa kabila la Manase, alishambulia vijiji kadhaa vya Gileadi na kuviteka, akavipa jina Hawoth-yairi. Naye Noba aliishambulia na kuiteka Kenathi na vijiji vyake, akauita Noba, jina lake mwenyewe. Vifuatavyo ni vituo ambavyo Waisraeli walipiga kambi walipotoka Misri wakiwa katika makundi ya makabila yao chini ya uongozi wa Mose na Aroni. Mose aliandika jina la kila mahali walipopiga kambi, kituo baada ya kituo, kwa agizo la Mwenyezi-Mungu. Waisraeli waliondoka mjini Ramesesi mnamo siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza, siku moja baada ya Pasaka ya kwanza. Waliondoka kwa uhodari mkubwa mbele ya Wamisri wote, ambao walikuwa wanawazika wazaliwa wao wa kwanza wa kiume aliowaua Mwenyezi-Mungu; kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa ameiadhibu hata miungu yao. Basi, Waisraeli waliondoka Ramesesi, wakapiga kambi yao huko Sukothi. Kutoka Sukothi, walipiga kambi yao huko Ethamu, ukingoni mwa jangwa. Kutoka Ethamu, waligeuka na kurudi hadi Pi-hahirothi, mashariki ya Baal-sefoni, wakapiga kambi yao karibu na Migdoli. Waliondoka Pi-hahirothi, wakapita bahari ya Shamu mpaka jangwa la Ethamu; walisafiri jangwani mwendo wa siku tatu, wakapiga kambi yao Mara. Kutoka Mara, walisafiri hadi Elimu; huko Elimu kulikuwa na chemchemi kumi na mbili za maji na mitende sabini, wakapiga kambi yao mahali hapo. Walisafiri kutoka Elimu, wakapiga kambi yao karibu na bahari ya Shamu. Kutoka Bahari ya Shamu walipiga kambi yao katika jangwa la Sini. Kutoka jangwa la Sini, walipiga kambi yao Dofka. Kutoka Dofka walipiga kambi yao huko Alushi. Kutoka Alushi walipiga kambi yao huko Refidimu, ambapo hapakuwa na maji ya kunywa. Waliondoka Refidimu wakapiga kambi yao katika jangwa la Sinai. Kutoka Sinai walipiga kambi yao huko Kibroth-hataava. Kutoka Kibroth-hataava, walipiga kambi yao huko Haserothi. Kutoka Haserothi, walipiga kambi yao huko Rithma. Kutoka Rithma, walipiga kambi yao huko Rimon-perezi. Kutoka Rimon-perezi, walipiga kambi yao huko Libna. Kutoka Libna walipiga kambi yao Risa. Waliondoka Risa, wakapiga kambi yao huko Kehelatha. Kutoka Kehelatha, walipiga kambi yao kwenye Mlima Sheferi. Kutoka Mlima Sheferi walipiga kambi yao huko Harada. Kutoka Harada, walipiga kambi yao huko Makelothi. Kutoka Makelothi, walipiga kambi yao huko Tahathi. Kutoka Tahathi walipiga kambi yao Tera. Kutoka Tera walipiga kambi yao Mithka. Kutoka Mithka, walipiga kambi yao Hashmona. Kutoka Hashmona, walipiga kambi yao Moserothi. Kutoka Moserothi, walipiga kambi yao Bene-yaakani. Kutoka Bene-yaakani, walipiga kambi yao Hor-hagidgadi. Kutoka Hor-hagidgadi, walipiga kambi yao Yot-batha. Kutoka Yot-batha, walipiga kambi yao Abrona. Kutoka Abrona, walipiga kambi yao Esion-geberi. Waliondoka Esion-geberi, wakasafiri na kupiga kambi yao katika jangwa la Sini, (yaani Kadeshi). Kutoka Kadeshi, walipiga kambi yao mlimani Hori, mpakani mwa nchi ya Edomu. Kwa agizo la Mwenyezi-Mungu kuhani Aroni alipanda juu ya Mlima Hori, na huko, akafariki mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa tano, mwaka wa arubaini tangu Waisraeli walipotoka nchini Misri. Aroni alikuwa na umri wa miaka 123 alipofariki juu ya Mlima Hori. Mfalme wa Aradi, Mkanaani, aliyekaa Negebu katika nchi ya Kanaani, alipata habari kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja. Kutoka Mlima Hori, Waisraeli walipiga kambi yao Salmona. Kutoka Salmona, walipiga kambi yao Punoni. Kutoka Punoni, walipiga kambi yao Obothi. Kutoka Obothi, walipiga kambi yao Iye-abarimu, katika eneo la Moabu. Kutoka Iye-abarimu, walipiga kambi yao Dibon-gadi. Kutoka Dibon-gadi, walisafiri na kupiga kambi yao Almon-diblathaimu. Kutoka Almon-diblathaimu, walisafiri na kupiga kambi yao katika milima ya Abarimu, karibu na Mlima Nebo. Kutoka milima ya Abarimu, walisafiri na kupiga kambi yao katika tambarare za Moabu ngambo ya mto Yordani karibu na Yeriko. Walipiga kambi hiyo karibu na mto Yordani kati ya Beth-yeshimothi na bonde la Abel-shitimu kwenye tambarare za Moabu. Katika tambarare za Moabu, ngambo ya mto Yordani karibu na Yeriko, Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli kwamba mtakapovuka mto Yordani na kuingia katika nchi ya Kanaani, wafukuzeni wenyeji wote wa nchi hiyo mbele yenu. Mtaziharibu sanamu zao zote za mawe na za kusubu na kupabomoa kila mahali pao pa juu pa ibada. Mtaichukua nchi hiyo na kukaa humo kwa sababu nimewapeni muimiliki. Mtaigawanya nchi hiyo kwa kura kufuata familia zenu; eneo kubwa kwa kabila kubwa na eneo dogo kwa kabila dogo. Lakini kama msipowafukuza wenyeji wa nchi hiyo kwanza, basi wale mtakaowaacha watakuwa kama vibanzi machoni mwenu au miiba kila upande, na watawasumbua. Nami nitawafanyeni nyinyi kama nilivyokusudia kuwafanya wao.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waamuru Waisraeli ukisema: Mtakapoingia Kanaani, nchi ambayo ninawapa iwe nchi yenu, mipaka ya eneo lenu lote itakuwa kama ifuatavyo. Upande wa kusini mpaka wenu utakuwa kutoka jangwa la Sini kupitia upande wa Edomu. Utaanzia mashariki upande wa kusini mwisho wa Bahari ya Chumvi. Kisha utapinda kusini kuelekea pito la Akrabimu na kupitia Sini hadi Kadesh-barnea, upande wa kusini. Kutoka hapo, mpaka utapinda kuelekea kaskazini-magharibi hadi Hasar-adari na kupita hadi Azmoni. Kutoka Azmoni utapinda kuelekea kijito cha Misri kwenye mpaka wa Misri na kuishia bahari ya Mediteranea. “Mpaka wenu wa upande wa magharibi utakuwa bahari ya Mediteranea. “Mpaka wenu wa upande wa kaskazini utakuwa kama ifuatavyo: Kutoka bahari ya Mediteranea, mtatia alama hadi Mlima Hori. Kutoka Mlima Hori mtatia alama hadi pito la Hamathi, na kuendelea hadi Sedadi, na kupita hadi Zifroni na kuishia Hazar-enani; huo utakuwa mpaka wenu wa kaskazini. “Mpaka wenu wa upande wa mashariki mtauweka kutoka Hazar-enani hadi Shefamu. Kutoka Shefamu utaelekea kusini hadi Ribla, mashariki mwa Aini; kisha mpaka huo utakwenda chini hadi mteremko wa mashariki wa ziwa Kinerethi, halafu utateremka kufuata mto Yordani hadi Bahari ya Chumvi; hii ndiyo itakuwa nchi yako kama mpaka ulivyo.” Basi, Mose akawaambia Waisraeli, “Hii ndiyo nchi mtakayoirithi kwa kupiga kura, nchi ambayo Mwenyezi-Mungu ameagiza yapewe makabila tisa na nusu. Kabila la Reubeni na la Gadi, na nusu ya kabila la Manase yamepata urithi wao kulingana na koo zao. Makabila hayo mawili na nusu yamepata urithi wao ngambo ya mto Yordani upande wa mashariki, mkabala wa Yeriko, mawioni.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kuhani Eleazari na Yoshua mwana wa Nuni ndio watakaowagawia watu nchi kuwa mali yao. Utachukua pia kiongozi mmoja kutoka kila kabila kusaidia katika ugawaji wa nchi. Haya ndiyo majina yao: Kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune. Kabila la Simeoni, Shemueli mwana wa Amihudi. Kabila la Benyamini, Elidadi mwana wa Kisloni. Kabila la Dani, Buki mwana wa Yogli. Kabila la Manase mwanawe Yosefu, Hanieli mwana wa Efodi. Kabila la Efraimu, mwanawe Yosefu, Kemueli mwana wa Shiftani. Kabila la Zebuluni, Elisafani mwana wa Parnaki. Kabila la Isakari, Paltieli mwana wa Azani. Kabila la Asheri, Ahihudi mwana wa Shelomi Kabila la Naftali, Pedaheli mwana wa Amihudi. Hawa ndio watu ambao Mwenyezi-Mungu aliwaamuru wawagawie Waisraeli nchi ya Kanaani kuwa mali yao.” Mwenyezi-Mungu aliongea na Mose katika tambarare za Moabu, ngambo ya mto Yordani karibu na Yeriko, akamwambia, “Waamuru Waisraeli kwamba kutokana na urithi watakaomiliki, wawape Walawi miji ya kukaa na sehemu za malisho kandokando ya miji hiyo. Miji hiyo itakuwa yao, nao watakaa humo na malisho yake yatakuwa kwa ajili ya ng'ombe na mifugo yao pamoja na wanyama wao wengine. Malisho ya maeneo mtakayowapa Walawi kandokando ya miji yataenea kila upande umbali wa mita 450 kutoka kwenye kuta za miji hiyo. Kwa hiyo, eneo hilo la malisho litakuwa la mita 900, na litaenea kila upande wa mji, mji wenyewe ukiwa katikati. Eneo hilo litakuwa malisho yao kandokando ya miji yao. Mtawapa Walawi miji sita ya makimbilio ambapo mtu akimuua mwenzake bila kukusudia ataruhusiwa kukimbilia. Pamoja na hiyo, mtawapa miji mingine arubaini na miwili. Jumla ya miji mtakayowapa Walawi itakuwa arubaini na minane; mtawapa miji hiyo pamoja na sehemu za malisho yake. Idadi ya miji mtakayowapa Walawi katika urithi wa Waisraeli itategemea ukubwa wa kabila; kabila kubwa litatoa miji mingi na kabila dogo litatoa michache. Kila kabila litatoa miji yake kwa ajili ya Walawi kulingana na eneo litakalorithi.” Mwenyezi-Mungu akaongea na Mose, akamwambia, Waambie Waisraeli kwamba wakati mtakapovuka mto Yordani na kuingia nchini Kanaani, mtachagua miji itakayokuwa miji ya makimbilio ambamo kama mtu akimuua mwenzake bila kukusudia ataweza kukimbilia. Miji hiyo itakuwa mahali pa kukimbilia usalama ili huyo mwuaji asiuawe na mwenye kulipiza kisasi kabla ya kuhukumiwa na jumuiya. Mtajitengea miji sita kwa ajili ya makimbilio. Kati ya miji hiyo sita mtakayoitenga, mitatu iwe mashariki ya Yordani, na mitatu iwe katika nchi ya Kanaani. Miji hii itakuwa ya makimbilio kwa ajili ya Waisraeli na wageni wa kudumu au wa muda wanaokaa pamoja nao. Mtu yeyote akimuua mwingine bila kukusudia anaweza kukimbilia huko. “Lakini mtu akimpiga mwenzake kwa kitu cha chuma, akafa, mtu huyo ni mwuaji na ni lazima auawe. Mtu yeyote akimpiga mwenzake kwa jiwe, akifa, mtu huyo ni mwuaji, na lazima auawe. Kama akimpiga mwenzake kwa silaha ya mti ambayo yaweza kusababisha kifo, akafa, mtu huyo ni mwuaji, na ni lazima auawe. Jamaa wa karibu wa mtu aliyeuawa atalipiza kisasi. Huyu atakapokutana na huyo mwuaji, atatekeleza hukumu ya kifo. “Hali kadhalika, kama mtu anamchukia mwenzake halafu, akamsukuma au kumtupia kitu kwa kumvizia, au kwa kumpiga ngumi akafa, basi mtu huyo aliyempiga mwenzake ni mwuaji na ni lazima auawe. Jamaa wa karibu wa mtu aliyeuawa atalipiza kisasi atakapokutana naye. “Lakini kama mtu akimsukuma mwenzake kwa ghafla bila chuki au kumtupia kitu bila kumvizia au mtu akirusha jiwe linaloweza kusababisha kifo, akamuua mtu bila kukusudia, ingawa hakuwa adui yake wala hakutaka kumdhuru, basi, jumuiya itaamua kati ya huyo mwuaji na jamaa ya mtu aliyeuawa anayetaka kulipiza kisasi, kulingana na sheria hizi. Jumuiya itamwokoa mtu huyo aliyeua mikononi mwa jamaa ya mtu aliyeuawa, na kumrudisha katika mji wa makimbilio alimokuwa amekimbilia. Atakaa huko mpaka kifo cha kuhani mkuu wa wakati huo aliyeteuliwa kwa kupakwa mafuta matakatifu. Lakini huyo aliyeua akitoka nje ya mji aliokimbilia wakati wowote ule, halafu jamaa ya mtu aliyeuawa akampata nje ya mipaka ya mji huo wa makimbilio akamuua, huyo hatakuwa na hatia ya kuua. Maana huyo aliyeua ni lazima akae ndani ya mji wa makimbilio mpaka kuhani mkuu atakapofariki; lakini baada ya kifo cha kuhani mkuu anaweza kurudi nyumbani. “Sheria hizi zitatumika katika vizazi vyenu vyote, mahali popote mtakapokaa. “Mtu yeyote atakayeua mtu, atahukumiwa kifo kutokana na ushahidi wa mashahidi wawili au zaidi; mtu yeyote hawezi kuhukumiwa kifo kutokana na ushahidi wa mtu mmoja. “Msipokee fidia yoyote kuokoa maisha ya mwuaji aliyepatikana na hatia, akahukumiwa kifo; mtu huyo lazima auawe. Msipokee wala msikubali fidia yoyote kutoka kwa mtu aliyekimbilia mji wa makimbilio ili kumruhusu arudi kukaa nyumbani kwake kabla ya kifo cha kuhani mkuu. Mkifanya hivyo mtakuwa mnaitia unajisi nchi ambayo mnakaa. Umwagaji damu huitia nchi unajisi, na hakuna sadaka iwezayo kuitakasa nchi iliyofanyiwa mauaji isipokuwa kwa kumuua mwuaji huyo. Msiitie unajisi nchi ambayo mnakaa, nchi ambayo mimi ninakaa; maana mimi Mwenyezi-Mungu ninakaa miongoni mwenu Waisraeli.” Viongozi wa jamaa katika ukoo wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, mwana wa Yosefu, walikwenda kuzungumza na Mose na viongozi wengine wa koo za Waisraeli. Wakasema, “Bwana wetu, Mwenyezi-Mungu alikuamuru kuwagawia watu wa Israeli nchi kwa kura, kuwa urithi wao; alikuamuru pia uwape binti za Selofehadi ndugu yetu urithi wa baba yao. Lakini wao wakiolewa na Waisraeli wa makabila mengine, urithi wao utatoka kwetu na kuwaendea watu wa kabila watakamoolewa; kwa hiyo urithi wetu sisi utapungua. Katika sikukuu ya ukumbusho urithi wao utahesabiwa pamoja na ule wa kabila watakamoolewa na hivyo kabila letu halitapata urithi huo tena.” Basi, Mose akawapa Waisraeli agizo lifuatalo kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, akawaambia, “Watu wa ukoo wa kabila la Yosefu, wamesema ukweli. Na hivi ndivyo anavyoamuru Mwenyezi-Mungu kuhusu binti za Selofehadi; wako huru kuolewa na mtu yeyote wampendaye, lakini waolewe katika kabila lao, ili urithi wa Waisraeli usihamishiwe kwa kabila lingine; kila Mwisraeli atazingatia urithi wa kabila lake. Mwanamke yeyote mwenye urithi katika kabila mojawapo la Israeli ni lazima aolewe na mtu wa kabila lake, ili kila Mwisraeli achukue urithi wa babu zake. Hivyo hapatakuwa na urithi wowote utakaohamishwa kutoka kabila moja hadi jingine. Kila kabila la Waisraeli litashikilia urithi wake.” Binti za Selofehadi walifanya kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Wote: Mala, Tirza, Hogla, Milka na Noa wakaolewa na binamu zao. Waliolewa katika jamaa za ukoo wa Manase mwana wa Yosefu, na urithi wao ukabaki katika kabila la baba yao. Hizo ndizo amri na maagizo ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli kwa njia ya Mose katika tambarare za Moabu, ngambo ya Mto Yordani karibu na mji wa Yeriko. Kitabu hiki kina maneno ambayo Mose aliwaambia watu wote wa Israeli wakati walipokuwa nyikani mashariki ya mto Yordani. Walikuwa katika bonde la Yordani karibu na Sufu, kati ya mji wa Parani upande mmoja na mji wa Tofeli, Labani, Hazerothi na Dizahabu, upande mwingine. (Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka mlima Horebu hadi Kadesh-barnea kwa njia ya mlima Seiri.) Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na moja, mwaka wa arubaini, baada ya kutoka Misri, Mose aliwaambia watu kila kitu ambacho Mwenyezi-Mungu alimwamuru awaambie. Alifanya hivyo baada ya kumshinda mfalme Sihoni wa Waamori ambaye alikuwa anakaa mjini Heshboni, na mfalme Ogu wa Bashani ambaye alikuwa anakaa mjini Ashtarothi na Edrei. Mose alichukua jukumu la kuwaelezea watu sheria ya Mungu wakati walipokuwa ngambo ya pili ya mto Yordani. Aliwaambia hivi: “Tulipokuwa mlimani Sinai, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu alituambia hivi: ‘Mmekaa muda wa kutosha kwenye mlima huu; sasa vunjeni kambi yenu mwendelee na safari. Nendeni kwenye nchi ya milima ya Waamori na maeneo ya nchi jirani katika Araba, kwenye milima na mabonde, huko Negebu na sehemu za pwani; naam, nendeni mpaka nchi ya Kanaani, na nchi ya Lebanoni, hadi kwenye ule mto mkubwa wa Eufrate. Nchi hii yote nimeiweka mbele yenu. Basi, nendeni mkaimiliki nchi hiyo ambayo mimi Mwenyezi-Mungu niliapa kuwapa wazee wenu Abrahamu, Isaka, Yakobo na wazawa wao.’” Mose akawaambia watu, “Tulipokuwa bado mlimani Sinai, mimi niliwaambieni hivi: ‘Jukumu la kuwaongozeni ni kubwa mno kwangu mimi peke yangu. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewafanya muwe wengi; leo mmekuwa wengi kama nyota za mbinguni. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, na awafanye mzidi kuongezeka mara elfu zaidi ya mlivyo sasa na kuwabariki kama alivyoahidi! Lakini mimi peke yangu nitawezaje kuchukua jukumu hilo zito la kusuluhisha ugomvi wenu? Chagueni kutoka katika kila kabila watu wenye hekima, busara na ujuzi ili niwateue wawe viongozi wenu.’ Nyinyi mlikubali, mkanijibu hivi: ‘Jambo ulilosema ni la busara’. Hivyo niliwachukua wale viongozi wenye hekima, busara na ujuzi ambao mliwachagua kutoka katika makabila yenu, nikawaweka kuwa viongozi wenu. Niliwaweka wengine kuwa makamanda wa makundi ya watu elfuelfu, ya watu miamia, ya watu hamsinihamsini na ya watu kumikumi. Nilichagua pia maofisa wengine wa kuchunga kila kabila. “Wakati huohuo niliwapa waamuzi wenu maagizo yafuatayo: ‘Sikilizeni kesi za watu wenu. Toeni hukumu za haki katika visa vya watu wenu, kadhalika na mizozo ya wageni waishio pamoja nanyi. Msimpendelee mtu yeyote katika kutoa hukumu; mtawasikiliza bila upendeleo, wakubwa kwa wadogo. Msitishwe na mtu yeyote, maana hukumu mnayotoa inatoka kwa Mungu. Kesi yoyote ikiwa ngumu zaidi kwenu, ileteni kwangu, nami nitaisikiliza.’ Wakati huohuo, niliwaagizeni mambo yote mnayopaswa kufanya. “Basi, kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru, tulianza safari yetu kutoka mlima Horebu, tukapita katika lile jangwa kubwa la kutisha mnalolijua, kwa kufuata njia inayoelekea nchi ya milima ya Waamori. Tulipofika Kadesh-barnea, mimi niliwaambieni: ‘Sasa mmefika katika nchi ya milima ya Waamori ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametupatia. Tazameni, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ameiweka nchi hii mbele yenu. Haya! Ingieni, mkaimiliki kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wenu alivyowaambia. Msiogope wala msifadhaike!’ “Kisha nyote mlikuja karibu nami mkaniambia, ‘Tutume watu watutangulie, waipeleleze nchi, halafu warudi kutujulisha njia bora ya kufuata na miji ipi tutaikuta huko.’ Jambo hilo lilionekana kuwa jema kwangu, nikawateua watu kumi na wawili, mtu mmoja kutoka katika kila kabila. Watu hao walikwenda katika nchi ile ya milima, wakafika kwenye bonde la Eshkoli na kulipeleleza. Waliporudi, walituletea baadhi ya matunda ya nchi hiyo na wakatuarifu kwamba nchi hiyo anayotupatia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ni nzuri. “Lakini nyinyi hamkufuata agizo la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kukataa kwenda katika nchi hiyo. Mlinungunika ndani ya mahema yenu mkisema, ‘Mwenyezi-Mungu anatuchukia na ndiyo maana alitutoa nchini Misri. Alitaka kututia mikononi mwa Waamori, atuangamize. Kwa nini tuende huko hali tumevunjika moyo kwa hofu? Wametuambia kuwa watu wa huko ni wakubwa na warefu kuliko sisi, na kwamba miji yao ni mikubwa na yenye kuta zifikazo mawinguni. Tena wamesema kwamba waliwaona wale wazawa wa Anaki!’ “Lakini mimi niliwaambieni hivi: ‘Msiwe na hofu wala msiwaogope watu hao.’ Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambaye huwatangulia, yeye mwenyewe atapigana kwa ajili yenu kama alivyofanya mbele yenu kule Misri na kule jangwani ambako mliona jinsi alivyowabeba safari hiyo yote kama vile baba amchukuavyo mwanawe mpaka mkafika hapa. Lakini japo nilisema hayo yote, nyinyi hamkumwamini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambaye aliwatangulia njiani na kuwatafutia mahali pa kupiga kambi zenu. Usiku aliwatangulieni kwa moto na mchana kwa wingu, ili kuwaonesha njia. “Mwenyezi-Mungu aliyasikia manunguniko yenu, akakasirika, akaapa akisema: ‘Hakuna hata mmoja wenu katika kizazi hiki kiovu atakayeingia katika nchi ile nzuri niliyoahidi kuwapa wazee wenu. Kalebu mwana wa Yefune, ndiye tu atakayeiona; nami nitampatia nchi hiyo aliyoikanyaga iwe yake yeye na wazawa wake kwa kuwa amekuwa mwaminifu kabisa kwangu.’ Mwenyezi-Mungu alinikasirikia mimi pia kwa sababu yenu, akasema, ‘Hata wewe Mose hutaingia katika nchi hiyo. Lakini msaidizi wako Yoshua mwana wa Nuni, ataingia humo. Basi, mtie moyo kwani yeye atawaongoza watu wa Israeli waimiliki nchi hiyo’. Kisha Mwenyezi-Mungu akatuambia sisi sote, ‘Hao watoto wenu mnaoogopa kwamba watakuwa nyara za adui zenu, naam hao walio wadogo ambao hawajui bado kupambanua kati ya mema na mabaya, hao ndio watakaoingia huko, nami nitawapa wao nchi hiyo iwe yao. Lakini nyinyi, geukeni na kurudi jangwani kuelekea Bahari ya Shamu.’ “Kisha mkanijibu, ‘Sisi tumemtendea dhambi Mwenyezi-Mungu, lakini sasa tutakwenda na kupigana kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru’. Hivyo, kila mmoja wenu akajitayarisha kupigana vita; maana mlifikiri kwamba lingekuwa jambo rahisi kuivamia nchi hiyo ya milima. Naye Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Waambie hao watu wasiende kupigana kwa sababu sipo pamoja nao; wasiende, wasije wakashindwa na adui zao’. Basi, mimi niliwaambieni hivyo, lakini nyinyi hamkusikia. Badala yake mlikataa kufuata agizo la Mwenyezi-Mungu, bila kujali mkaingia katika nchi hiyo ya milima. Hapo, Waamori waliokuwa wanaishi katika eneo hilo la milimani wakateremka kuwashambulia na kama wafanyavyo nyuki wakawapiga huko Seiri mpaka Horma. Ndipo mliporudi, mkamlilia Mwenyezi-Mungu, lakini Mwenyezi-Mungu hakuwasikiliza wala hakuwajali. Basi, mkabaki huko Kadeshi kwa muda mrefu ambao mlikaa huko. “Kisha, tuligeuka, tukasafiri jangwani kwa kupitia njia ya Bahari ya Shamu, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniambia; tulitangatanga karibu na mlima Seiri kwa muda mrefu. Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Mmetangatanga vya kutosha katika nchi hii ya milima; sasa geukeni mwelekee kaskazini. Mko karibu kupita katika nchi ya milima ya Seiri, nchi ya ndugu zenu wazawa wa Esau. Hao watawaogopeni, lakini muwe na tahadhari, msipigane nao kwa sababu sitawapeni sehemu yoyote ya nchi yao. Sitawapeni hata mahali padogo pa kukanyaga. Nchi hiyo ya milima ya Seiri nimewapa wazawa wa Esau iwe mali yao. Mkitaka chakula au maji kutoka kwao, lazima mnunue.’ “Basi, kumbukeni jinsi Mwenyezi-Mungu Mungu wenu alivyowabariki katika kila jambo mlilofanya. Aliwatunza mlipokuwa mnatangatanga katika jangwa hili kubwa. Amekuwa pamoja nanyi miaka hii yote arubaini na hamkupungukiwa kitu chochote. “Hivyo tuliendelea na safari yetu, tukawapita ndugu zetu, wazawa wa Esau ambao waliishi Seiri, tukaiacha nyuma ile njia ya Araba na pia miji ya Elathi na Esion-geberi. Kisha tukageuka tukafuata njia ya kupitia nyika ya Moabu. Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Usiwasumbue watu wa Moabu, wala usipigane nao maana sitawapeni sehemu yoyote ya nchi yao. Ila eneo hilo la Ari nimewapa hao wazawa wa Loti liwe mali yao.’ (Hapo zamani hiyo nchi ya Ari ilikuwa imekaliwa na watu wengi, wenye nguvu na ambao walikuwa warefu kama Waanaki. Kama vile Waanaki, watu hawa walijulikana pia kama Warefai, lakini Wamoabu waliwaita Waemi. Wahori pia waliishi huko Seiri hapo awali, lakini wazawa wa Esau waliwafukuza na kuwaangamiza, kisha wao wenyewe wakakaa katika eneo hilo badala yao. Waisraeli walifanya vivyo hivyo katika nchi ile ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa iwe mali yao). “Mwenyezi-Mungu akatuambia: ‘Ondokeni sasa, mvuke kijito Zeredi’. Basi, tukavuka kijito cha Zeredi. Miaka thelathini na nane ilikuwa imepita tangu kuondoka Kadesh-barnea mpaka kuvuka kijito cha Zeredi. Wakati huo, kizazi chote cha wale watu wa umri wa kwenda vitani kilikuwa kimetoweka kulingana na jinsi Mwenyezi-Mungu alivyowaapia. Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwakabili ili kuwaangamiza huko kambini, hata wote wakaisha. “Basi, watu hao wote wenye umri wa kwenda vitani walipokwisha aga dunia, Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Leo hii mtauvuka mpaka wa Moabu kwa kupitia nchi ya Ari. Mtaifikia nchi ya Waamoni. Msiwasumbue wala msipigane nao kwa kuwa sitawapeni sehemu yoyote ya hao wazawa wa Amoni; iwe mali yenu. La! Hao ni wazawa wa Loti, na nimewapa hiyo nchi iwe mali yao.’” (Nchi hiyo inajulikana pia kama nchi ya Warefai. Warefai walikuwa wanaishi huko hapo zamani; Waamoni waliwaita hao Wazamzumi. Walikuwa watu wengi, wenye nguvu na warefu kama Waanaki. Lakini Mwenyezi-Mungu aliwaangamiza walipofika Waamori ambao walichukua nchi yao wakaishi humo badala yao. Mwenyezi-Mungu alifanya kama alivyowafanyia wazawa wa Esau, Waedomu, ambao wanaishi katika nchi ya Seiri. Aliwaangamiza Wahori wakati Waedomu walipofika huko, wakainyakua nchi yao na kuishi humo hadi leo. Waavi walikuwa hapo awali wakiishi katika vijiji vya mwambao wa Mediteranea mpaka Gaza. Wakaftori kutoka kisiwa cha Kaptori wakawaangamiza, wakaishi humo badala yao). “Kisha Mwenyezi-Mungu alituamuru: ‘Haya! Anzeni safari. Vukeni bonde la Arnoni. Mimi nimemtia mikononi mwenu Sihoni, mfalme wa Waamori wa Heshboni na nchi yake. Mshambulieni na kuanza kuimiliki nchi yake. Leo nitaanza kuwafanya watu wote duniani wawe na woga na hofu juu yenu; watasikia habari zenu nao watatetemeka na kufadhaika.’ “Basi, nikatuma watu kutoka jangwa la Kedemothi waende kwa mfalme Sihoni wa Heshboni na ujumbe ufuatao wa amani: ‘Turuhusu tupite katika nchi yako. Tutapitia barabarani na kwenda moja kwa moja bila kugeuka kulia wala kushoto. Chakula chetu tutakinunua kwako na maji ya kunywa pia. Tunachoomba tu ni ruhusa ya kupita kwa miguu nchini mwako, tuvuke mto Yordani na kuingia katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu anatupatia. Wazawa wa Esau wanaoishi Seiri na Wamoabu waishio Ari walituruhusu pia kupita katika nchi yao’. “Lakini Sihoni, mfalme wa Heshboni, hakuturuhusu tupite nchini mwake. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alimfanya awe na kichwa kigumu na mkaidi wa moyo, ili tumshinde na kuchukua nchi yake ambayo tunaimiliki hadi leo. “Halafu Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Tazama, nimeanza kumtia mfalme Sihoni na nchi yake mikononi mwenu; anzeni kuichukua nchi yake na kuimiliki’. Kisha Sihoni alitoka na watu wake wote kupigana nasi karibu na mji wa Yahasa. Naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, akamtoa, tukamshinda yeye, watoto wake na watu wake wote. Tukaiteka na kuiharibu miji yake yote, tukaua wanaume na wanawake na watoto; hatukumwacha mtu yeyote hai. Nyara zetu zilikuwa tu mifugo na mali yote tuliyokuta mijini. Kuanzia Aroeri, mji ulio ukingoni mwa bonde la Arnoni na mji ulio ndani ya bonde hili mpaka Gileadi, hakuna mji wowote uliokuwa imara hata tukashindwa kuuteka. Mwenyezi-Mungu aliitia yote mikononi mwetu. Lakini hatukukaribia nchi ya Waamoni au ukingoni mwa mto Yaboki wala katika miji ya nchi ya milima wala sehemu yoyote ile ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alitukataza. “Kisha, tuligeuka, tukapanda kuelekea Bashani. Mfalme Ogu alitoka na watu wake wote kupigana nasi karibu na mji wa Edrei. Lakini Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Usimwogope, maana nimemtia mikononi mwako pamoja na watu wake na nchi yake. Utamtendea kama ulivyomtendea Sihoni mfalme wa Waamori aliyekaa kule Heshboni’. “Basi, Mwenyezi-Mungu alimtia mikononi mwetu mfalme Ogu wa Bashani na watu wake, tukawaangamiza hata asibakie mtu yeyote. Tuliiteka miji yake yote; hakuna hata mji mmoja ambao hatukuuteka. Jumla tuliiteka miji sitini, yaani eneo lote la Argobu ambalo lilitawaliwa na mfalme Ogu wa Bashani. Miji yote hii ilikuwa na ngome zenye kuta ndefu, zilizokuwa na malango na makomeo. Kulikuwa pia na vijiji vingi ambavyo havikuzungukwa na kuta. Tuliteketeza kila kitu huko, tukaharibu kila mji na kuua wanaume, wanawake na watoto kama tulivyofanya katika miji ya mfalme Sihoni wa Heshboni. Lakini mifugo yote na mali tulichukua nyara. “Wakati huo tuliitwaa nchi hiyo ya wale wafalme wawili wa Waamori waliokuwa wanakaa ngambo ya mto Yordani, katikati ya mto Arnoni na mlima Hermoni. (Wasidoni huuita mlima huo Sirioni, nao Waamori huuita Seniri). Tuliiteka miji yote katika sehemu tambarare za mwinuko, na pia eneo lote la Gileadi na Bashani mpaka Saleka na Edrei, miji ya mfalme Ogu huko Bashani.” (Mfalme Ogu ndiye peke yake aliyesalia miongoni mwa Warefai. Kitanda chake kilichotengenezwa kwa chuma, kilikuwa na urefu wa mita nne na upana wa karibu mita mbili, kadiri ya vipimo vya kawaida. Kitanda hicho bado kipo katika mji wa Waamori wa Raba.) “Tulipoitwaa nchi hiyo, niliwapa makabila ya Reubeni na Gadi eneo la kuanzia kaskazini mwa Aroeri karibu na Arnoni na nusu ya eneo la milima ya Gileadi, pamoja na miji yake. Kisha nililipatia nusu ya lile kabila la Manase sehemu iliyobaki ya Gileadi pamoja na Bashani yote iliyotawaliwa na Ogu, yaani eneo lote la Argobu. (Nchi yote ya Bashani ilijulikana kama nchi ya Warefai.) Yairi, mtu wa kabila la Manase, alichukua eneo lote la nchi ya Argobu, yaani Bashani, hadi kwenye mpaka wa Geshuri na Maaka. Vijiji vyote alivipa jina lake, na hadi leo vinajulikana kama vijiji Hawoth-yairi. Watu wa ukoo wa Makiri wa kabila la Manase niliwapa Gileadi, na watu wa makabila ya Reubeni na Gadi niliwapa nchi yote kutoka Gileadi hadi mto Arnoni. Mpaka wao wa kusini ulikuwa katikati ya mto na wa kaskazini ulikuwa mto Yaboki ambao ndio unaopakana na nchi ya Waamori. Upande wa magharibi nchi yao ilienea hadi mto Yordani, toka ziwa Galilaya upande wa kaskazini, ukashuka hadi bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, mpaka miteremko ya Pisga, upande wa mashariki. “Wakati ule niliwapa maagizo haya: ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapeni nchi hii mashariki ya mto Yordani iwe mali yenu. Sasa nyinyi mashujaa kati ya ndugu zenu, chukueni silaha mvuke mto Yordani mkiwa mbele ya ndugu zenu Waisraeli. Lakini wake zenu, watoto wenu na wanyama wenu, najua mnayo mifugo mingi, watabaki kwenye miji niliyowapeni. Wasaidieni ndugu zenu Waisraeli mpaka Mwenyezi-Mungu atakapowajalia watulie mahali pao kama nanyi mlivyotulia, yaani nao pia waimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapatia huko ngambo ya Yordani. Baada ya hayo, mtaweza kurejea katika nchi yenu hii ambayo nimewapeni iwe yenu!’ “Kisha nikamwamuru Yoshua, ‘Wewe umeona kwa macho yako mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amewatendea wafalme hawa wawili, Sihoni na Ogu; basi, yeye atawatendea vivyo hivyo wafalme wa nchi zote mtakazopitia. Msiwaogope maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye atakayepigana kwa ajili yenu.’ “Wakati huo nilimsihi Mwenyezi-Mungu nikisema, ‘Ee Bwana, Mwenyezi-Mungu, ninajua umenionesha mimi mtumishi wako mwanzo tu wa ukuu wako na uwezo wako. Maana, kuna mungu gani huko mbinguni au duniani awezaye kufanya mambo makuu na ya ajabu kama ulivyofanya wewe? Nakuomba nivuke mto Yordani, niione nchi hiyo nzuri magharibi ya Yordani; naam, nchi nzuri ya kupendeza ya milima, pamoja na milima ya Lebanoni’. “Lakini Mwenyezi-Mungu alinikasirikia kwa sababu yenu, akakataa kunisikiliza. Badala yake aliniambia, ‘Inatosha! Usiseme tena jambo hili. Panda mpaka kilele cha mlima Pisga, utazame vizuri upande wa magharibi, kaskazini, kusini na mashariki, na kuiona nchi hiyo; ila wewe hutavuka huu mto wa Yordani. Lakini mpe Yoshua maagizo, umtie moyo na kumuimarisha, maana yeye ndiye atakayewaongoza watu hawa hadi ngambo, kuimiliki nchi utakayoiona’. “Basi, tukabaki hapa bondeni mbele ya Beth-peori.” Mose akaendelea kusema, “Zingatieni basi na kufuata masharti yote na maagizo niliyowafundisha, ili mpate kuishi na kumiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, anawapeni. Msiongeze chochote katika amri ninazowapeni, wala msipunguze kitu; zingatieni amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambazo ninawapeni. Nyinyi mliona kwa macho yenu mambo ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafanya kuhusu Baal-peori. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwaangamiza watu wote miongoni mwenu waliomwabudu huyo mungu Baal-peori. Lakini nyinyi mliokuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mko hai hadi leo. “Haya! Nimewafundisheni masharti na maagizo kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, alivyoniamuru nifanye, ili muyazingatie katika nchi mnayokwenda kuimiliki. Shikeni na kuyatekeleza masharti na maagizo hayo maana mkifanya hivyo watu wa mataifa mengine watakapopata kujua masharti hayo, watatambua kuwa nyinyi ni wenye hekima na busara, wakisema: ‘Kweli watu wa taifa hili kuu wana hekima na busara!’ “Hakuna taifa lolote hata liwe kuu namna gani, ambalo mungu wake yuko karibu nalo, kama alivyo karibu nasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, tunapomwomba msaada. Wala hakuna taifa lingine lolote hata liwe kuu namna gani, lenye masharti na maagizo ya haki, kama hayo ambayo nimewafundisha siku hii ya leo. “Lakini muwe waangalifu na kujihadhari sana msije mkasahau mambo yale mliyoyaona kwa macho yenu wenyewe. Isije ikatokea hata mara moja maishani mwenu mambo hayo yakasahaulika mioyoni mwenu. Wasimulieni watoto wenu na wajukuu wenu juu ya siku ile ambayo mlisimama mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kule Horebu, aliponiambia, ‘Wakusanye hao watu mbele yangu, niwaambie maneno yangu ili wajifunze kunicha mimi siku zote za maisha yao, na kuwafundisha watoto wao kufanya hivyo’. “Basi, mlikaribia na kusimama chini ya ule mlima ambao wakati huo ulikuwa unawaka moto uliofika mpaka mbinguni ukiwa umetanda giza na wingu zito. Kisha Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi kutoka katikati ya moto huo; mliyasikia maneno aliyosema lakini hamkumwona; mlisikia tu sauti yake. Naye akawatangazia agano lake akawaamuru mlishike yaani mzitii zile amri kumi ambazo aliziandika juu ya vibao viwili vya mawe. Wakati huo Mwenyezi-Mungu aliniamuru niwafundishe masharti na maagizo yote ambayo mnapaswa kuyatekeleza katika nchi mnayokwenda kuimiliki. “Kwa hiyo muwe waangalifu msije kusahau kwamba: Mwenyezi-Mungu alipoongea nanyi kule mlimani Horebu katikati ya moto hamkumwona kwa umbo. Kwa sababu hiyo jihadharini sana, msipotoke kwa kujifanyia sanamu yoyote ya kuchonga, au ya umbo au mfano wowote, mfano wa kiume au wa kike, wa mnyama yeyote duniani au ndege, au mfano wa mnyama atambaaye ardhini au wa samaki majini. Jihadharini ili wakati mtakapoangalia na kutazama jua, mwezi na nyota na jeshi lote la mbinguni, msije mkashawishiwa kuviabudu na kuvitumikia, maana vitu hivyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliviumba kwa ajili ya watu wote duniani. Lakini nyinyi ndio watu aliowakomboa kutoka Misri katika tanuri la chuma. Aliwatoeni huko ili muwe watu wake kama vile mlivyo hivi leo. Kwa sababu yenu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alinikasirikia, akaapa kwamba mimi sitavuka mto Yordani kuingia katika nchi ile nzuri anayowapeni iwe mali yenu. Mimi nitafia katika nchi hii wala sitauvuka mto, lakini nyinyi mko karibu kuuvuka na kwenda kuimiliki nchi ile nzuri. Jihadharini sana msije mkasahau agano ambalo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amefanya nanyi; msijifanyie sanamu ya kuchonga katika umbo la kitu chochote ambacho Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewakataza kumfananisha, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni moto uteketezao; yeye ni Mungu mwenye wivu. “Mtakapokuwa mmekaa katika nchi hiyo, mkapata watoto na wajukuu na kuwa wazee, kama mkianza kupotoka na kujifanyia sanamu ya kuchonga katika umbo la kitu chochote, mkafanya uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kumkasirisha, basi, mimi leo naziita mbingu na dunia zishuhudie kati yenu; nawaambieni kwamba mara moja mtaangamia kabisa katika nchi ambayo mnaenda kuimiliki huko ngambo ya mto Yordani. Hamtaishi huko muda mrefu, bali mtaangamizwa kabisa. Mwenyezi-Mungu atawatawanya kati ya mataifa mengine, na ni wachache wenu tu watakaosalia huko ambako Mwenyezi-Mungu atawafukuzia. Huko mtaitumikia miungu ya miti na mawe ambayo imetengenezwa kwa mikono ya watu; na ambayo haiwezi kuona, haisikii, haili wala kunusa. Kisha kutoka humohumo nchini mtamtafuta Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nanyi mtampata kama mkimtafuta kwa moyo wote na roho yote. Mambo haya yote yatakapowapata huko baadaye, mkapata taabu, mtamrudia Mwenyezi-Mungu na kumtii. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni Mungu mwenye rehema, hatawaacheni wala kuwaangamiza, wala kusahau agano ambalo alifanya na wazee wenu kwa kiapo. “Fikirini sana juu ya matukio ya zamani, mambo yaliyotukia kabla nyinyi hamjazaliwa, tangu siku ile Mungu alipomuumba mtu duniani. Ulizeni ulimwenguni kote, toka pembe moja hadi nyingine, kama jambo la ajabu la namna hii limepata kutokea au kusikika! Je, watu walikwisha sikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama nyinyi mlivyosikia, wakabaki hai? Je, kuna Mungu yeyote mwingine aliyejaribu kamwe kwenda kujichukulia taifa lake kutoka taifa jingine, kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyofanya, kwa kutumia majaribio, ishara na maajabu, kwa vita na kwa nguvu yake kuu, akasababisha mambo ya kutisha ambayo nyinyi mlishuhudia kwa macho yenu kule Misri? Nyinyi mlijaliwa kuyaona mambo hayo, ili mpate kutambua kwamba Mwenyezi-Mungu, ndiye peke yake Mungu na wala hakuna mwingine. Aliwafanya muisikie sauti yake kutoka mbinguni ili aweze kuwafunza nidhamu; na hapa duniani akawafanya mwone moto wake mkubwa na kusikia maneno yake kutoka katikati ya moto huo. Kwa kuwa aliwapenda wazee wenu, yeye amewateua nyinyi wazawa wao, akawatoa yeye mwenyewe nchini Misri kwa nguvu yake kuu. Aliyafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi, ili awalete na kuwapeni nchi yao iwe urithi wenu, kama ilivyo hadi leo! Basi, kumbukeni leo na kuweka mioyoni mwenu, kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu juu mbinguni na chini duniani; hakuna mwingine. Kwa hiyo shikeni masharti yake na amri zake ambazo ninawapeni leo ili mfanikiwe, nyinyi pamoja na wazawa wenu, na kuishi siku nyingi katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni iwe yenu milele.” Ndipo Mose akatenga miji mitatu mashariki ya mto Yordani, ambamo mtu ataweza kukimbilia na kujisalimisha, kama ameua mtu ambaye si adui yake kwa bahati mbaya. Mtu kama huyo ataweza kukimbilia katika mji mmojawapo na kuyaokoa maisha yake. Alitenga mji wa Beseri katika tambarare ya jangwa kwa ajili ya kabila la Reubeni; mji wa Ramothi katika nchi ya Gileadi kwa ajili ya kabila la Gadi, na mji wa Golani katika nchi ya Bashani kwa ajili ya kabila la Manase. Hii ndiyo sheria ambayo Mose aliwapa Waisraeli. Haya ndiyo maamuzi, masharti na maagizo ambayo Mose aliwaambia Waisraeli walipotoka Misri, wakiwa ngambo ya mto Yordani, katika bonde lililo mbele ya Beth-peori, katika nchi iliyokuwa ya mfalme Sihoni wa Waamori, aliyetawala kutoka mjini Heshboni, ambaye Mose na Waisraeli walimshinda walipotoka Misri. Waliitwaa nchi yake na nchi ya mfalme Ogu wa Bashani. Wafalme hao wawili wa Waamori walitawala huko mashariki ya mto Yordani. Nchi hiyo ilienea toka Aroeri ukingoni mwa mto Arnoni, hadi mlima Sirioni yaani Hermoni, pamoja na eneo lote mashariki ya mto Yordani mpaka bahari ya Araba, mwishoni mwa miteremko ya mlima Pisga. Mose aliwaita pamoja Waisraeli, akawaambia: “Enyi Waisraeli, sikilizeni masharti na maagizo ambayo ninayatamka mbele yenu leo. Jifunzeni hayo na kuyatekeleza kwa uangalifu. Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alifanya agano nasi mlimani Horebu. Hakufanya agano hilo na wazee wetu tu, bali alifanya na sisi sote ambao tuko hai hivi leo. Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi ana kwa ana huko mlimani katikati ya moto. Wakati huo mimi nilisimama kati yenu na Mwenyezi-Mungu, nikawatangazieni yale aliyoyasema, kwa kuwa nyinyi mliogopa ule moto na hamkupanda mlimani. Mwenyezi-Mungu alisema hivi, “ ‘Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri, ambako ulikuwa mtumwa. “ ‘Usiwe na miungu mingine ila mimi. “ ‘Usijifanyie sanamu za miungu za kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. “ ‘Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu. Nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wale wanichukiao. Lakini nawafadhili maelfu ya wale wanipendao na kuzishika amri zangu. “ ‘Usilitaje bure jina langu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; maana mimi ni Mwenyezi-Mungu sitaacha kumwadhibu yeyote afanyaye hivyo. Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka wakfu, kama mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nilivyokuamuru. Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote, lakini siku ya saba ni siku ya Sabato ambayo imetengwa kwa ajili yangu. Siku hiyo wewe usifanye kazi yoyote, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika vilevile kama wewe. Usisahau kwamba wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, nami Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nikakutoa huko kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyoshwa; ndiyo maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako nimekuamuru kuiadhimisha siku ya Sabato. “ ‘Waheshimu baba yako na mama yako, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako nilivyokuamuru; fanya hivyo ili uishi siku nyingi na kufanikiwa katika nchi ambayo ninakupatia. “ ‘Usiue. “ ‘Usizini. “ ‘Usiibe. “ ‘Usimshuhudie jirani yako uongo. “ ‘Usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba yake, wala shamba lake, wala mtumwa wake wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kitu chochote alicho nacho jirani yako.’ “Hizi ndizo amri Mwenyezi-Mungu alizowaambieni nyote kwa sauti kubwa kutoka katika moto na lile wingu zito na giza nene. Aliwaambieni mlipokuwa mmekusanyika kule mlimani na hakuongeza hapo amri nyingine. Kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe, akanipatia. “Wakati mliposikia hiyo sauti kutoka katikati ya lile giza, juu ya ule mlima uliokuwa unawaka moto, viongozi wote wa makabila yenu na wazee walinijia wakasema, ‘Sikiliza! Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametufunulia utukufu na ukuu wake; tumeisikia sauti yake kutoka katikati ya ule moto. Leo hivi tumemwona Mungu akiongea na binadamu, naye binadamu badala ya kufa akaendelea kuishi! Lakini ya nini kujitia katika hatari ya kufa kwa kuteketezwa na ule moto mkubwa? Tukiisikia tena sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, tutakufa! Je, ni binadamu gani aliyepata kumsikia Mungu aliye hai akiongea kutoka katikati ya moto kama tulivyomsikia sisi halafu akaweza kubaki hai? Heri wewe Mose uende karibu, ukasikilize yote atakayosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kisha uje kutuambia mambo hayo yote atakayokuambia. Sisi tutayasikiliza na kuyatekeleza’. “Mwenyezi-Mungu alisikia maneno yenu hayo, akaniambia ‘Nimesikia maneno waliyokuambia watu hawa; yote waliyosema ni sawa. Laiti wangekuwa daima na mawazo kama haya wakaniheshimu na kushika amri zangu! Mambo yao yote yangewaendea vyema daima wao wenyewe na wazawa wao milele. Nenda ukawaambie warudi mahemani mwao. Lakini wewe Mose usimame hapa karibu nami; mimi nitakuambia amri zote na masharti na maagizo ambayo utawafundisha, ili nchi ambayo ninawapa iwe mali yao.’ “Nyinyi muwe waangalifu mkafanye kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru; tekelezeni kila kitu barabara. Mtafuata njia yote Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyowaamuru kufuata ili mambo yenu yawaendee vyema na mpate kuishi muda mrefu katika nchi mtakayotwaa iwe mali yenu. “Hizi ndizo amri, masharti na maagizo ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliniamuru niwafundishe, ili muyatekeleze katika nchi mnayokwenda kuimiliki. Wakati wote mlipo hai, mtapaswa kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuzitii kanuni zote na amri ninazowapeni nyinyi na wazawa wenu ili mpate kuishi maisha marefu. Kwa hiyo enyi Waisraeli, muwe waangalifu kuzitekeleza ili mfanikiwe na kuongezeka sana katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali kama alivyowaahidi. “Basi sikilizeni enyi Waisraeli! Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni Mwenyezi-Mungu mmoja. Mpendeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa moyo wenu wote, kwa roho yenu yote na kwa nguvu zenu zote. Wekeni mioyoni mwenu maneno hayo ninayowaamuru leo na kuwafundisha kwa uangalifu watoto wenu. Mtawasimulia muwapo mnakaa nyumbani au mlipo safarini au mnapolala au mnapoamka. Yafungeni katika mikono yenu na kuyavaa katika vipaji vya nyuso zenu kama ukumbusho. Yaandikeni kwenye miimo ya milango yenu na malango ya miji yenu. “Kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaapia babu zenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo, yeye atawapeni nchi yenye miji mikubwa na mizuri iliyostawi ambayo nyinyi hamkuijenga. Nyumba zitakuwa zimejaa vitu vizuri ambavyo nyinyi hamkuviweka, kutakuwa na visima ambavyo hamkuvichimba na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hamkuyapanda. Mwenyezi-Mungu atakapowapeleka kwenye nchi hiyo ambako mtakuwa na chakula chote mnachohitaji, hakikisheni kwamba hamtamsahau Mwenyezi-Mungu aliyewatoa Misri ambako mlikuwa watumwa. Mtamcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mtamtumikia yeye peke yake na kuapa kwa jina lake peke yake. Msiabudu miungu mingine, miungu ya watu walio jirani nanyi, hasira ya Mwenyezi-Mungu isije ikawaka juu yenu, naye akawafutilia mbali kutoka duniani, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliye kati yenu, ni Mungu mwenye wivu. “Msimjaribu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu kule Masa. Hakikisheni kwamba mnazitii amri zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, maamuzi na masharti yake ambayo amewaamuru. Fanyeni yale yanayompendeza Mwenyezi-Mungu, ili mpate kufanikiwa. Mtaweza kuimiliki nchi ile nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu aliapa kuwapa babu zenu, na kwamba Mwenyezi-Mungu atawafukuza adui zenu kama alivyoahidi. “Siku zijazo, watoto wenu wakiwauliza, ‘Nini maana ya maamuzi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, aliwaamuru kutenda?’ Nyinyi mtawajibu hivi: ‘Sisi tulikuwa watumwa wa Farao, mfalme wa Misri, na Mwenyezi-Mungu akatuokoa kwa mkono wake wenye nguvu. Kwa macho yetu wenyewe tulimwona akifanya ishara na miujiza na mambo ya kutisha na ya ajabu dhidi ya Wamisri, mfalme wao na wakuu wake. Alitutoa Misri, akatuleta hapa na kutupa nchi hii, kama alivyoapa kwamba atawapa babu zetu. Basi, Mwenyezi-Mungu alituamuru kuzitii kanuni hizi zote na kumcha kwa faida yetu wenyewe; apate kutulinda daima kama hivi leo. Tena tutakuwa waadilifu kama tukitimiza kwa uangalifu amri hizi zote mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama alivyotuamuru’. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawafikisha kwenye nchi ambayo mtakwenda kufanya makao yenu na atayafukuza mataifa mengi kutoka nchi hiyo. Mtakapoingia, atayafukuza mbele yenu mataifa saba makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi: Wahiti, Wagirgashi, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Pia, baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuyatia mikononi mwenu, mkawashinda watu hao na kuwaangamiza kabisa, msifanye agano lolote nao wala msiwahurumie. Msioane nao, wala msiwaoze binti zenu au wana wenu kwao. Mkifanya hivyo wao watawapotosha watoto wenu wasimfuate Mwenyezi-Mungu, na kuwafanya waabudu miungu mingine, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu itawaka juu yenu, halafu atawaangamiza mara moja. Lakini watendeni hivi: Mtazivunjilia mbali madhabahu zao na kuzibomoa nguzo zao. Na sanamu za Ashera mtazikatilia mbali na kuzitia moto sanamu zao za kuchonga. Fanyeni hivyo kwa kuwa nyinyi mmewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kati ya watu wote ulimwenguni aliwachagua nyinyi ili muwe taifa lake mwenyewe. “Mwenyezi-Mungu hakuwapenda nyinyi na kuwateua kwa kuwa nyinyi ni wengi mno kuliko watu wengine; nyinyi mlikuwa wachache kuliko mataifa mengine duniani. Lakini ni kwa sababu Mwenyezi-Mungu anawapenda na anashika kiapo alichowaapia babu zenu, ndiyo maana aliwaokoeni kwa mkono wake wenye nguvu na kuwaokoa toka utumwani, toka mikono ya Farao mfalme wa Misri. Basi, jueni kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayeshika agano lake na huwaonesha fadhili kwa vizazi vingi vya wale wanaoshika amri zake. Lakini huwalipa wanavyostahili wale wanaomchukia, wala hatasita kuwaadhibu wanaomchukia. Kwa hiyo muwe waangalifu kushika amri, masharti na maagizo ninayowaamuru leo. “Mkisikiliza maagizo haya na kuyashika hata kuyatenda, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atashika agano lake nanyi na atawaonesheni fadhili kama alivyowaahidi babu zenu. Atawapenda na kuwabariki, nanyi mtaongezeka na kuwa na wazawa wengi; atayabariki mashamba yenu ili mpate nafaka, divai na mafuta; atawabariki kwa kuwapeni ng'ombe na kondoo wengi katika nchi aliyowaahidi babu zenu kuwa atawapeni nyinyi. Mtabarikiwa kuliko watu wengine wote ulimwenguni. Miongoni mwenu hakutakuwa na mwanamume wala mwanamke tasa. Mwenyezi-Mungu atawaondoleeni magonjwa yote na hamtapatwa na magonjwa yoyote ya kutisha kama yaliyowapata huko Misri, lakini atawapa maadui zenu magonjwa hayo. Angamizeni taifa lolote ambalo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; atalitia mikononi mwenu, wala msilionee huruma. Msiabudu miungu yao, kwani jambo hili litakuwa mtego kwenu. “Msijisemee mioyoni mwenu: ‘Watu hawa ni wengi kuliko sisi, twawezaje kuwafukuza nchini?’ Msiwaogope, kumbukeni vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyomtendea Farao na nchi nzima ya Misri. Kumbukeni maradhi mabaya mliyoyaona kwa macho yenu, miujiza na maajabu na nguvu kubwa na uwezo mkuu, ambavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; alitumia kuwakomboa; hivyo ndivyo atakavyowatenda watu mnaowaogopa. Zaidi ya hayo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atapeleka mavu kati yao na kuwaangamiza wale ambao watawatoroka ili kujificha. Basi, msiwaogope, kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, yuko kati yenu. Yeye ni Mungu mkuu na wa kutisha. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atayafukuza mataifa haya kadiri mnavyosonga mbele kidogokidogo. Hamtaweza kuyaangamiza yote kwa mara moja, kwa sababu mkifanya hivyo idadi ya wanyama wa porini itazidi na kuwa tisho kwenu. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawatia adui zenu mikononi mwenu na atawafanya wahangaike mpaka waangamie. Atawatia wafalme wao mikononi mwenu. Mtawaua, nao watasahaulika. Hakuna mtu yeyote atakayeweza kuwazuia, mpaka mtakapowaangamiza. Teketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga za miungu yao. Msitamani fedha wala dhahabu yao, wala msiichukue na kuifanya mali yenu. Kufanya hivyo ni mtego kwenu na ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Msipeleke nyumbani kwenu kitu chochote cha kuchukiza, la sivyo mtalaaniwa kama hicho kitu. Ni lazima mkichukie na kukidharau kabisa kwa kuwa ni kitu kilicholaaniwa. “Amri zote ninazowapeni leo, lazima mzifuate kwa uangalifu ili mpate kuishi na kuongezeka, mpate kuingia na kuimiliki ile nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliapa kuwapa babu zenu. Kumbukeni jinsi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaongoza katika safari ndefu kupitia jangwani kwa muda wa miaka hiyo arubaini, ili awatweze na kuwajaribu ili ajue mliyokuwa mnawaza mioyoni mwenu, na kama mngezishika amri zake au la. Aliwanyenyekesha, akawaacha muone njaa na baadaye akawapa mana mle, chakula ambacho hamkukijua, wala babu zenu hawajapata kukijua. Alifanya hivyo ili apate kuwafundisha kuwa binadamu haishi kwa mkate tu, bali kwa kila asemalo Mwenyezi-Mungu. Wakati huo wa miaka arubaini nguo zenu hazikuchakaa, wala miguu yenu haikuvimba. Kumbukeni kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawarudi kama vile baba amrudivyo mwanawe. Hivyo, shikeni amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mpate kuzifuata njia zake na kumcha yeye. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawaleteni kwenye nchi nzuri, nchi yenye vijito na chemchemi, na maji yabubujikayo kutoka bondeni na milimani; nchi yenye ngano na shayiri, mizabibu, mitini, mikomamanga, mizeituni na asali. Huko mtapata chakula tele na hamtapungukiwa kitu. Miamba yake ina chuma, na kwenye milima yake mnaweza kuchimba shaba. Mtakula na kushiba, mtamshukuru Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa nchi nzuri aliyowapa. “Hakikisheni kwamba hamtamsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kutoshika amri zake, maagizo yake na masharti yake ninayowaamuru leo. Mkisha kula mkashiba, mkajijengea nyumba nzuri na kuishi humo, na wakati ambapo ng'ombe na kondoo wenu, dhahabu na fedha yenu, na kila kitu mlicho nacho kitakuwa kimeongezeka, msiwe na kiburi na kumsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, mahali mlipokuwa watumwa. Ndiye aliyewaongoza katika lile jangwa kubwa na la kutisha, lenye nyoka wenye sumu na nge; katika nchi ile kame isiyokuwa na maji, aliwatolea maji kutoka kwenye mwamba mgumu. Tena ndiye aliyewalisheni mana jangwani, chakula ambacho babu zenu hawakupata kukijua. Alifanya hayo yote ili awanyenyekeshe na kuwajaribu, ili kuwapima apate kuwajalia mema mwishowe. Hivyo jihadharini msije mkajisemea mioyoni mwenu: ‘Tumejitajirisha kwa uwezo na nguvu zetu wenyewe’. Kumbukeni kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye awapaye uwezo wa kupata utajiri. Anafanya hivyo ili kuimarisha agano alilofanya na babu zenu mpaka leo. Lakini mkimsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuifuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, nawaonyeni vikali leo hii kuwa hakika mtaangamia. Msipomtii Mwenyezi-Mungu, mtaangamia kama mataifa ambayo anayaangamiza mbele yenu. “Sikilizeni enyi Waisraeli! Hivi leo mmekaribia kuvuka mto Yordani, kwenda kumiliki nchi ya mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi. Miji yao ni mikubwa na ina kuta zifikazo mawinguni. Watu wenyewe ni warefu na wenye nguvu; ni Waanaki ambao kama mjuavyo na kama mlivyosikia watu husema juu yao ‘Nani awezaye kuwakabili?’ Jueni leo hii kwamba anayewatangulia kama moto uteketezao miti ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Yeye atawaangamiza hao na kuwashinda mbele yenu; kwa hiyo mtawafukuza na kuwaangamiza mara moja, kama Mwenyezi-Mungu alivyowaahidi. “Baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuwafukuza watu hao mbele yenu, msiseme moyoni mwenu kuwa, ‘Ni kwa sababu ya uadilifu wetu Mwenyezi-Mungu ametuleta tuimiliki nchi hii,’ ambapo Mwenyezi-Mungu amewafukuza watu hawa mbele yenu kwa sababu wao ni waovu. Mnaweza kuimiliki nchi yao si kwa sababu nyinyi ni watu wema au wenye mioyo safi; bali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawafukuza watu hao mbele yenu kwa sababu ni waovu na anataka kuliweka imara lile neno alilowaapia babu zenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo. Basi, jueni ya kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni nchi hii nzuri mwimiliki si kwa sababu mnastahili kuimiliki, maana nyinyi ni watu wakaidi. “Kumbukeni na msisahau jinsi mlivyomkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kule jangwani. Tangu siku ile mlipotoka nchi ya Misri mpaka siku mlipofika mahali hapa, nyinyi mmekuwa mkimwasi Mwenyezi-Mungu. Hata huko mlimani Horebu, mlimkasirisha Mwenyezi-Mungu, naye alikasirika sana, kiasi cha kutaka kuwaangamiza. Nilipopanda mlimani kupokea vibao vya mawe ambavyo viliandikwa agano ambalo Mwenyezi-Mungu alifanya nanyi, nilikaa huko siku arubaini, usiku na mchana; sikula wala kunywa chochote. Kisha Mwenyezi-Mungu alinipa vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole chake Mungu; vilikuwa vimeandikwa maneno yote ambayo Mwenyezi-Mungu aliwaambieni mlimani kutoka kwenye moto siku ya mkutano. Naam, baada ya siku hizo arubaini, usiku na mchana, Mwenyezi-Mungu alinipa vibao hivyo viwili vya mawe ambavyo viliandikwa agano. “Basi, Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Ondoka, ushuke chini ya mlima upesi, kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamepotoka. Wameiacha upesi njia niliyowaamuru wafuate na wamejifanyia sanamu ya kusubu’. “Kadhalika, Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Nimewaona watu hawa, ni watu wakaidi sana; niache niwaangamize, nilifutilie mbali jina lao duniani; nami nitakufanya wewe kuwa taifa lenye nguvu na kubwa kuliko wao.’ “Basi, niligeuka, nikashuka kutoka mlimani, nikiwa nimebeba vile vibao viwili vya mawe, nao moto ulikuwa unawaka mlimani. Nilitazama, nikaona kwamba tayari mmekwisha kutenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; mlikwisha jitengenezea sanamu ya ndama ya kusubu; bila kukawia mlikwisha iacha njia ya Mwenyezi-Mungu ambayo aliwaamuru. Hivyo, nilivishika vile vibao viwili nikavitupa chini, nikavivunja mbele yenu. Kisha nikalala chini kifudifudi mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama hapo awali, kwa muda wa siku arubaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji, kwa sababu ya dhambi mliyokuwa mmetenda kwa kufanya maovu mbele yake Mwenyezi-Mungu kwa kumkasirisha. Niliogopa kwamba hasira na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu dhidi yenu, ingewaangamiza; lakini Mwenyezi-Mungu alinisikiliza pia wakati huo. Hali kadhalika, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemkasirikia sana Aroni, kiasi cha kumwangamiza; hivyo, nikamwombea Aroni wakati huohuo. Kile kitu kiovu, yaani yule ndama mliyejitengenezea, nilikichukua, nikakiteketeza motoni, nikakipondaponda na kukisagasaga, kikawa mavumbi laini; halafu nikayatupa hayo mavumbi kwenye kijito kilichotiririka chini ya mlima huo. “Pia mlimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, huko Tabera, Masa na Kibroth-hataava. Na Mwenyezi-Mungu alipowatuma kutoka Kadesh-barnea akisema, ‘Nendeni mkaimiliki nchi ambayo nimewapatia,’ mlimwasi; hamkusadiki wala hamkutii yale aliyowaambia. Nyinyi mmekuwa waasi dhidi ya Mwenyezi-Mungu tangu siku nilipowajua. “Kwa hiyo, nililala kifudifudi mbele ya Mwenyezi-Mungu siku hizo arubaini, usiku na mchana, kwa sababu Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema atawaangamiza. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, nikisema. ‘Ee Mwenyezi-Mungu, usiwaangamize watu wako na urithi wako, watu uliowakomboa na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa uwezo na nguvu yako kubwa. Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, Isaka na Yakobo, wala usiujali ukaidi, uovu na dhambi za watu hawa. Watu wa kule ulikotutoa wasije wakasema, Mwenyezi-Mungu aliwatoa ili awaue jangwani kwa sababu hakuweza kuwaingiza katika nchi aliyowaahidi na kwa sababu aliwachukia. Maana, hawa ni watu wako na urithi wako; watu ambao uliwatoa kutoka Misri kwa nguvu na uwezo wako mkuu.’ “Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, na sanduku la mbao, halafu uje kwangu huku juu mlimani, nami nitaandika maneno yaliyokuwa yameandikwa katika vibao vile ulivyovunja, kisha viweke vibao hivyo katika sanduku’. “Basi, nikatengeneza sanduku la mshita na vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nikavitwaa mkononi, nikapanda navyo mlimani. Mwenyezi-Mungu akaandika katika vibao hivyo maneno yaleyale kama ya hapo awali: Amri kumi ambazo aliwapeni alipoongea kutoka katika moto siku ya mkutano. Halafu Mwenyezi-Mungu akanipa vibao hivyo. Niligeuka, nikashuka kutoka mlimani, na kama Mwenyezi-Mungu alivyoniagiza, niliviweka vibao hivyo ndani ya sanduku nililokuwa nimelitengeneza, na vimo ndani ya sanduku hilo, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniamuru.” (Watu wa Israeli walisafiri kutoka visima vya watu wa Yaakani hadi Mosera. Hapo, Aroni alifariki, akazikwa. Eleazari mwanawe, akachukua nafasi yake kama kuhani. Kutoka hapo, walisafiri hadi Gudgoda, na kutoka Gudgoda hadi Yot-batha, eneo lenye vijito vingi vya maji. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu aliwateua watu wa kabila la Lawi wawe wakilibeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, wamtumikie kama makuhani na kubariki watu kwa jina lake hata hivi leo. Ndio maana kabila la watu wa Lawi halina sehemu ya nchi ya urithi pamoja na ndugu zao; walichopokea ni heshima ya kuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu, kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyoahidi). “Nilikaa mlimani kwa muda wa siku arubaini, usiku na mchana, kama hapo awali. Mwenyezi-Mungu alinisikiliza kwa mara nyingine tena na akakubali kwamba hatawaangamiza. Kisha akaniambia ‘Ondoka uendelee na safari yako ukiwaongoza watu ili waweze kuingia na kuimiliki nchi niliyowaapia babu zenu ya kuwa nitawapa’. “Sasa, enyi Waisraeli, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anataka nini kwenu, ila kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuzifuata njia zake zote, kumpenda, kumtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote, na kuzitii amri na masharti ya Mwenyezi-Mungu ninayowawekea leo, kwa manufaa yenu wenyewe? Tazama, mbingu hata mbingu za mbingu ni mali yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; dunia na vyote vilivyomo ni mali yake. Tena Mwenyezi-Mungu aliwapenda babu zenu kwa dhati, akawachagua nyinyi wazawa wao kuwa watu wake badala ya watu wengine wote, kama ilivyo hivi leo. Kwa hiyo, takaseni mioyo yenu, msiwe wakaidi tena. Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana. Yeye ni Mungu mkuu na mwenye nguvu, na wa kuogofya; hapendelei wala hapokei rushwa. Huwapa haki yatima na wajane; huwapenda wageni na kuwapa chakula na nguo. Basi, wapendeni wageni kwa kuwa nanyi pia mlikuwa wageni nchini Misri. Mcheni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; mtumikieni; ambataneni naye na kuapa kwa jina lake. Yeye ni fahari yenu; ndiye Mungu wenu ambaye amewatendea haya mambo makubwa na ya kutisha mliyoyaona kwa macho yenu wenyewe. Babu zenu walipokwenda Misri, walikuwa watu sabini tu, lakini sasa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi kama nyota za mbinguni. “Kwa ajili hiyo, mpendeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kushika siku zote kanuni zake, masharti yake, maagizo yake na amri zake. Fikirini kwa makini, kwa sababu ya watoto wenu ambao hawakujua wala hawakuona adhabu ya Mwenyezi-Mungu, uwezo wake na nguvu zake, ishara zake na maajabu yake aliyoyatenda kule Misri kwa Farao mfalme wa Misri na nchi yake yote; aliyoyatendea majeshi ya Misri, farasi wao na magari yao ya vita, jinsi alivyozamisha jeshi hilo katika bahari ya Shamu, na jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoliangamiza hata hivi leo. Pia kumbukeni aliyowafanyieni Mwenyezi-Mungu jangwani kabla hamjafika hapa, na mambo aliyowatenda Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, mwana wa Reubeni; jinsi mbele ya watu wote wa Israeli nchi ilivyofunuka na kuwameza pamoja na jamaa zao, mahema yao, wanyama na watumishi wao wote. Maana macho yenu yameona matendo yote haya makubwa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafanya. “Tiini amri zote ninazowaamuru siku hii ya leo, ili muweze kuingia na kuimiliki nchi mnayoiendea, mpate kuishi kwa muda mrefu katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali; nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliahidi kuwapa babu zenu na wazawa wao. Kwa kuwa nchi mnayokwenda kuimiliki si kama nchi ya Misri mlikotoka, ambako mlipanda nafaka, mkamwagilia maji kwa miguu kama mashamba ya mboga. Lakini nchi mnayokwenda kuimiliki, ni nchi ya milima na mabonde, nchi ambayo hupata maji ya mvua kutoka mbinguni, nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, huitunza; Mwenyezi-Mungu huiangalia daima tangu mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka. “Basi, mkizitii amri zangu ninazowapeni leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkamtumikia kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote, yeye ataipatia mvua nchi yenu wakati wake, mvua za masika na mvua za vuli, nanyi mtavuna nafaka yenu, divai yenu na mafuta yenu. Ataotesha majani mashambani kwa ajili ya ng'ombe wenu, nanyi mtakula na kushiba. Jihadharini, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi yenu, akazifunga mbingu hata pasiwepo mvua na nchi ikaacha kutoa mazao yake, halafu mkaangamia upesi kutoka katika nchi nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu anawapa. “Yawekeni maneno yangu haya mioyoni mwenu na rohoni mwenu. Yafungeni mikononi mwenu kama alama na kuyavaa katika paji la uso. Wafundisheni watoto wenu maneno haya mkiyazungumzia mketipo katika nyumba zenu, mnapotembea, mnapolala na mnapoamka. Ziandikeni katika vizingiti vya nyumba zenu, na katika malango yenu, ili nyinyi na watoto wenu mpate kuishi maisha marefu katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliapa kuwapa babu zenu, siku zote mbingu zitakapodumu juu ya dunia. “Mkijihadhari kutenda amri zote ambazo nimewapa: Kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuzifuata njia zake zote na kuambatana naye, basi Mwenyezi-Mungu atayafukuza mataifa yote hayo mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi iliyo mali ya mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi. Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; nchi yenu itaenea kutoka jangwani, upande wa kusini, hadi milima ya Lebanoni upande wa kaskazini, na kutoka mto Eufrate upande wa mashariki, hadi bahari ya Mediteranea upande wa magharibi. Hakuna mtu yeyote atakayeweza kuwakabili. Popote mtakapokwenda katika nchi hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawatia watu hofu wawaogope, kama alivyowaahidi. “Angalieni, leo hii nawawekea mbele yenu baraka na laana: Baraka, kama mtatii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambazo nawapeni hivi leo; na laana, kama hamtazitii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuiacha njia ninayowaamuru, mkaabudu miungu mingine ambayo hata hamjawahi kuijua. Mwenyezi-Mungu atakapowafikisha kwenye nchi mnayokwenda kuimiliki, mtatangaza baraka kutoka mlima Gerizimu, na laana kutoka mlima Ebali. (Milima hii iko ngambo ya mto Yordani, magharibi ya barabara kuelekea machweo ya jua, katika nchi ya Wakanaani waishio Araba mkabala wa Gilgali). Itawabidi kuvuka mto Yordani mwingie kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni. Basi, mtakapoimiliki na kukaa humo, muwe waangalifu kutimiza masharti yote na maagizo ninayowapa leo. “Yafuatayo ni masharti na maagizo ambayo mtayatimiza katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, amewapa muimiliki, siku zote za maisha yenu nchini. Haribuni kabisa mahali pote ambapo watu wanaabudu miungu yao kwenye milima mirefu, vilima na chini ya miti yenye majani mabichi. Zivunjilieni mbali madhabahu zao na kuzibomoa kabisa nguzo zao. Ziteketezeni kwa moto sanamu zao za Ashera na kuzikatakata sanamu zao za kuchonga na kufutilia mbali jina lao na mahali hapo. “Wala msimwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, namna hiyo yao. Bali mtakwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atachagua katika makabila yote ili kuliweka jina lake na makao yake hapo; huko ndiko mtakakokwenda. Huko mtapeleka tambiko zenu za kuteketezwa na sadaka zenu, zaka zenu za matoleo yenu, sadaka zenu za nadhiri, matoleo yenu ya hiari na wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na kondoo wenu. Huko, mtakula mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na mtafurahi nyinyi pamoja na watu wa nyumbani mwenu kwa ajili ya mafanikio yenu aliyowabarikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Msifanye kama tunavyofanya sasa, kila mtu kama apendavyo mwenyewe; kwa sababu bado hamjaingia mahali pa kupumzikia na katika urithi anaowapeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Lakini mtakapovuka mto Yordani na kuishi katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa mu irithi, na atakapowapatia pumziko msisumbuliwe na adui zenu wote watakaowazunguka ili muishi salama, basi huko mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapochagua ili jina lake likae, hapo ndipo mtakapopeleka kila kitu ninachowaamuru: Tambiko zenu za kuteketeza na sadaka zenu, zaka zenu na matoleo yenu, na sadaka zenu za nadhiri mnazoahidi kumtolea Mwenyezi-Mungu. Huko mtafurahi mbele yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi pamoja na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu wa kiume na wa kike, na Walawi wanaoishi katika miji yenu, maana wao hawana sehemu wala urithi kati yenu. Jihadharini msitoe sadaka zenu za kuteketezwa mahali popote mnapopaona; bali katika mahali atakapopachagua Mwenyezi-Mungu katika mojawapo ya makabila yenu. Hapo ndipo mtakapotoa sadaka zenu za kuteketezwa, na ndipo mtakapofanyia mambo yote niliyowaamuru. “Lakini mna uhuru wa kuchinja na kula wanyama wenu popote katika makao yenu mnavyopenda, kama baraka za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alizowapa, kadiri mtakavyojaliwa na Mwenyezi-Mungu. Watu wote, walio safi au najisi wanaweza kula nyama hizo, kama vile mlavyo nyama ya paa au ya kulungu. Lakini msile damu ya wanyama hao; imwageni damu hiyo ardhini kama maji. Msile vitu vifuatavyo mahali mnapoishi: Zaka ya nafaka zenu, wala ya divai yenu, wala ya mafuta yenu, wala ya wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe au kondoo wenu, wala sadaka zenu za nadhiri au tambiko zenu za hiari, wala matoleo mengineyo. Mtavila vitu hivyo mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mtavila nyinyi pamoja na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu wa kiume na wa kike, na Walawi wanaoishi katika miji yenu. Pia hakikisheni kwamba hamtawasahau Walawi muda wote mtakaoishi katika nchi yenu. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapoipanua nchi yenu, kama alivyoahidi, nanyi mtasema, ‘Tutakula nyama’, kwa vile mnapenda kula nyama, mnaweza kula nyama kiasi chochote mnachotaka. Basi, mahali atakapochagua Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aweke jina lake, hapo mnaweza kuchinja ng'ombe au kondoo yeyote ambaye Mwenyezi-Mungu amewajalia, kama nilivyowaamuru, na mnaweza kula kiasi chochote mnachotaka cha nyama hiyo, kama mkiwa katika miji yenu. Mtaila nyama hiyo kama aliwavyo paa au kulungu. Mtu yeyote anaweza kula, aliye safi na asiye safi. Ila hakikisheni kwamba hamli damu, maana damu ni uhai; hivyo basi, msile uhai pamoja na nyama. Msile damu hiyo, bali imwageni chini kama maji. Msile damu, nanyi mtafanikiwa pamoja na wazawa wenu, maana mtakuwa mnatenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu. Vitu vitakatifu mtakavyotoa na sadaka zenu za nadhiri, mtavichukua na kuvipeleka mahali Mwenyezi-Mungu atakapochagua. Hapo, mtatoa sadaka za kuteketezwa, nyama na damu, kwenye madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; damu ya mnyama mtainyunyiza kwenye madhabahu yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, lakini mnaruhusiwa kula nyama. Jihadharini kutii maneno haya niliyowaamuru, ili mpate kufanikiwa nyinyi pamoja na wazawa wenu baada yenu milele, maana mtakuwa mnatenda yaliyo mema na yaliyo sawa mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuyakatilia mbali mataifa mbele yenu, hayo ambayo mnakwenda kuyafukuza, kuyatoa na kukaa katika nchi yao, jihadharini msijiingize mtegoni kwa kuyafuata baada ya kuangamizwa mbele yenu. Msijisumbue kujua kuhusu miungu yao, mkisema, ‘Mataifa haya yaliabuduje miungu yake? — ili nasi tuwaabudu vivyo hivyo’. Msimwabudu hivyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa maana kila chukizo ambalo Mwenyezi-Mungu hapendi, wameifanyia miungu yao; hata wamewachoma motoni watoto wao wa kiume na wa kike, ili kuitambikia miungu yao. “Hakikisheni kwamba mmefanya kila kitu nilichowaamuru; msiongeze kitu wala msipunguze kitu. “Akitokea nabii au mtabiri wa ndoto miongoni mwenu, akawaahidi na kuwapa ishara au maajabu fulani, halafu ishara au maajabu hayo yatokee, kisha aseme: ‘Tufuate miungu mingine na kuitumikia, (miungu ambayo hamjapata kuijua)’, msisikilize maneno yake nabii huyo au mtabiri wa ndoto, kwa maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawatumia wao kuwajaribu, ili ajue kama mnampenda yeye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote. Mfuateni na kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kushika amri zake na kuitii sauti yake; mtumikieni na kuambatana naye. Lakini nabii huyo au mtabiri wa ndoto atauawa, kwa sababu atakuwa amewafundisha uasi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka utumwani, ili muiache njia ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliwaamuru muifuatea. Hivyo ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu. “Ikiwa ndugu yako wa tumbo moja, au mtoto wako wa kiume au wa kike, au mke wako umpendaye sana, au rafiki yako mwandani, atakushawishi kwa siri akisema, ‘Twende tukaabudu miungu mingine’, miungu ambayo wewe wala babu zenu hamuijui, au baadhi ya miungu ya watu wanaoishi karibu nanyi, au miungu ya watu waishio mbali toka ncha moja ya dunia hadi nyingine, usikubali kushawishiwa, wala usimsikilize au kumhurumia, wala usimwachilie wala kumficha; bali utamuua. Wewe utakuwa wa kwanza kuchukua hatua ya kumuua, kisha watu wengine wote watafuata. Mpigeni mawe mpaka afe! Kwa sababu amejaribu kukuvutia mbali na Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, aliyekutoa utumwani nchini Misri. Hivyo, Waisraeli wote watasikia na kuogopa, na kamwe hawatafanya uovu kama huo. “Mtakapoishi katika miji ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapa, huenda mkasikia kuwa watu fulani mabaradhuli miongoni mwenu, wamewashawishi watu wa mji wakisema, ‘Twende tukaabudu miungu mingine,’ miungu ambayo bado hamjawahi kuijua, basi mtapeleleza na kufanya uchunguzi na kuuliza kwa makini; na kama ni kweli kuwa jambo la kuchukiza limetendeka kati yenu, hamna budi kuwaua kwa upanga watu wa mji huo; mtauangamiza kabisa mji huo na kuwaua ng'ombe wote kwa upanga. Mtakusanya nyara zake zote katika uwanja wa hadhara wa mji na kuzichoma kwa moto kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana Mungu wenu; mji huo utakuwa rundo la magofu milele, nao hautajengwa tena. Msichukue kitu chochote kilichotolewa kiteketezwe, ili Mwenyezi-Mungu aache ile hasira yake kali, awaoneshe rehema na huruma, na kuwafanya muwe wengi sana kama alivyowaahidi babu zenu, kama tu mtaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkishika amri zake zote ninazowapa hivi leo, na kufanya yaliyo sawa mbele yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Nyinyi ni watoto wa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; msijichanje wala kunyoa upara kwa ajili ya mtu aliyefariki. Nyinyi ni watu watakatifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; Mwenyezi-Mungu amewachagua muwe watu wake hasa, kati ya watu wote waishio duniani. “Msile kitu kilicho chukizo kwa Mungu. Mnaweza kula wanyama wafuatao: Ng'ombe, kondoo, mbuzi, kulungu, paa, kongoni, mbuzimwitu, paa mweupe, pofu na mbuzi wa mlimani; na kila mnyama mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na mwenye kucheua, huyo mnaweza kula. Lakini msile mnyama yeyote ambaye kwato zake hazikugawanyika sehemu mbili na hacheui; msile ngamia, sungura na pelele, ingawa hucheua lakini kwato zao hazikugawanyika sehemu mbili; hao ni najisi kwenu. Pia msile nguruwe, maana ijapokuwa kwato zake zimegawanyika sehemu mbili, yeye hacheui; hao ni najisi kwenu, msile nyama zao wala msiguse mizoga yao. “Mnaweza kula kila aina ya samaki wenye mapezi na magamba. Lakini kiumbe chochote kinachoishi majini kisicho na mapezi wala magamba msile; hivyo ni najisi kwenu. “Mnaweza kula ndege wote walio safi. Lakini msile ndege wafuatao: Furukombe, kipungu, kengewa, kozi, mwewe kwa aina zake, kunguru kwa aina zake, mbuni, kirukanjia, dudumizi, kipanga kwa aina zake, bundi, mumbi, bundi mkubwa, mwari, nderi, mnandi, membe, koikoi kwa aina zake, hudihudi na popo. Na wadudu wote wenye mabawa ni najisi kwenu; msiwale. Mnaweza kula viumbe vyote vyenye mabawa vilivyo safi. Msile nyamafu yoyote; mnaweza kumpa mgeni anayeishi katika miji yenu, ale, au mnaweza kumwuzia mtu wa taifa lingine, kwa sababu nyinyi ni watakatifu na Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu. Msimchemshe mwanambuzi katika maziwa ya mama yake. “Toeni sehemu moja ya kumi ya mazao yenu yote ya shambani kila mwaka. Halafu nendeni mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amepachagua kuweka jina lake, na mkiwa mbele yake mtaila zaka ya nafaka yenu, ya divai yenu na ya mafuta, na ya wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na kondoo wenu; fanyeni hivi ili mjifunze kumcha Mwenyezi-Mungu Mungu wenu daima. Ikiwa safari ni ndefu kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amechagua mahali pa kuweka jina lake ambapo ni mbali mno na nyumbani, nanyi hamwezi kubeba zaka za mazao yenu ambayo Mwenyezi-Mungu amewajalia kupata, basi, fanyeni hivi: “Uzeni mazao yenu na kuchukua fedha hiyo mpaka mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alipopachagua, mzitumie hizo fedha kwa chochote kile mtakachopenda — nyama ya ng'ombe, nyama ya kondoo, divai au kinywaji kikali; mtavila na kufurahi hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, pamoja na jamaa zenu. Msiwasahau Walawi wanaoishi miongoni mwenu; wao hawana fungu wala urithi wao kati yenu. Na kila mwisho wa mwaka wa tatu toeni zaka ya mazao yenu yote na kuyaweka akiba katika miji yenu. Hiyo itakuwa kwa ajili ya Walawi, kwa kuwa hawana fungu wala urithi wao kati yenu, nao wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu, watakuja kula na kushiba. Fanyeni hivi naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, awabariki katika kazi zenu zote mfanyazo kwa mikono yenu. “Kila mwisho wa mwaka wa saba mtawasamehe wadeni wenu wote. Hivi ndivyo mtakavyofanya: Kila mmoja aliyemkopesha jirani yake, alifute hilo deni, wala asijaribu kumdai kwa sababu Mwenyezi-Mungu mwenyewe ameamua deni hilo lifutwe. Mnaweza kuwadai wageni, lakini madeni yote ya ndugu zenu wenyewe mtayafuta. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika nchi anayowapa iwe mali yenu. Hakuna hata mmoja atakayekuwa maskini kati yenu, mradi tu mumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kufuata kwa uangalifu amri ninazowapeni hivi leo. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawabariki kama vile alivyowaahidi. Nanyi mtayakopesha mataifa mengi, lakini nyinyi hamtakopa. Kadhalika mtatawala mataifa mengi, lakini mataifa hayo hayatawatawala nyinyi. “Kukiwa na maskini wa jamaa yenu katika miji ya nchi ambayo Mwenyezi-Mungu atawapa, msiwe wachoyo na wagumu kwake. Badala yake, fumbueni mikono yenu na kumkopesha kwa hiari kiasi cha kutosha mahitaji yake. Angalieni wazo ovu lisiwaingie mioyoni mwenu, mkasema: ‘Mwaka wa saba, mwaka wa kusamehe wadeni, uko karibu’; mkamfikiria ndugu yenu maskini kwa ukali na kukataa kumpa chochote; yeye aweza kumlilia Mwenyezi-Mungu dhidi yenu na hiyo ikawa dhambi kwenu. Mpeni ndugu maskini kwa ukarimu bila kunungunika; maana kwa ajili ya hayo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika kazi zenu zote na katika kila mfanyalo. Maana maskini hawatakosekana nchini; hivyo nawaamuru, muwe wakarimu kwa ndugu zenu wahitaji na maskini nchini mwenu. “Kama nduguyo Mwebrania, mwanamume au mwanamke, akiuzwa kwako, atakutumikia kwa miaka sita, lakini katika mwaka wa saba, utamwacha huru. Nawe utakapomwacha huru, usimwache aende mikono mitupu. Mpe kwa ukarimu kile ambacho Mwenyezi-Mungu amekubariki: Kondoo, nafaka na divai. Kumbukeni kwamba nyinyi mlikuwa watumwa huko Misri na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwakomboa; ndiyo maana leo nawaamuru hivyo. Lakini akikuambia, ‘Sitaondoka kwako,’ kwa sababu anakupenda wewe na jamaa yako na anaridhika kuishi nawe, basi, utachukua shazia na kutoboa sikio lake mpaka hiyo shazia iingie mlangoni naye atakuwa mtumwa wako milele. Kadhalika mtendee vivyo hivyo mtumwa wako wa kike. Wala usione ugumu utakapomwacha huru mtumwa wako, maana, amekutumikia kwa muda wa miaka sita kwa nusu ya ujira wa mtumishi wa kuajiri. Fanya hivyo, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atakubariki kwa kila utakalofanya. “Mtolee Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa kundi lako la ng'ombe na kondoo. Usiwafanyize kazi ng'ombe hao na kondoo hao usiwakate manyoya. Kila mwaka, wewe na jamaa yako mtakula wanyama hao mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mahali Mwenyezi-Mungu atakapochagua. Lakini mnyama huyo akiwa na dosari yoyote, yaani akiwa kilema au kipofu, au ana kasoro yoyote kubwa, usimtoe kuwa sadaka kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Utamla mnyama wa namna hiyo ukiwa katika mji wako; pia wote walio safi na wasio safi wanaweza kumla kama unavyokula paa au kulungu. Lakini usile damu yake; bali hiyo utaimwaga chini kama maji. “Adhimisheni mwezi wa Abibu na kufanya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Maana katika mwezi huo wa Abibu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliwatoa Misri wakati wa usiku. Mtatoa sadaka ya Pasaka kutoka mifugo yenu ya kondoo au ng'ombe kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu atachagua likae jina lake. Msile sadaka hiyo na mikate iliyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso — kwa sababu mlitoka Misri kwa haraka; kwa hiyo, muda wote mtakaoishi mtakumbuka ile siku mlipotoka Misri. Kwa muda wa siku saba mtu yeyote katika nchi yenu asiweke chachu nyumbani mwake; na nyama ya yule mnyama aliyechinjwa jioni ya siku ya kwanza isibaki mpaka asubuhi. Msitolee sadaka ya Pasaka katika mji wowote ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa, bali mtaitolea pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atapachagua likae jina lake, hapo ndipo mtakapotolea sadaka ya Pasaka jioni, jua linapotua, wakati uleule mlipotoka Misri. Hiyo nyama mtaichemsha na kuila mahali pale Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atakapochagua; asubuhi yake mtageuka na kurudi mahemani mwenu. Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu; na mnamo siku ya saba utakuwapo mkutano mkubwa wa kumwabudu Mwenyezi-Mungu, na msifanye kazi yoyote siku hiyo. “Mtahesabu majuma saba; mtaanza kuyahesabu tangu mnapoanza kuvuna nafaka. Halafu mtaadhimisha sikukuu ya majuma kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kutoa sadaka ya hiari, mtakayotoa kadiri awabarikiavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mtafurahia mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi pamoja na wana wenu na binti zenu, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi pamoja nanyi. Fanyeni haya katika mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapochagua likae jina lake. Mkumbuke kuwa mlikuwa watumwa kule Misri; basi muwe waangalifu kufuata masharti haya. “Baada ya kupura nafaka yenu yote na kukamua zabibu zenu, adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa muda wa siku saba. Mtafanya sherehe hiyo, nyinyi na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao huishi katika miji yenu. Kwa siku saba mtamfanyia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, sherehe mahali ambapo Mwenyezi-Mungu atapachagua; kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki kwa mazao yenu yote na katika shughuli zenu zote nanyi hakika mtafurahi. “Wanaume wote wa taifa lenu watakuja mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mara tatu kila mwaka, mahali atakapopachagua: Wakati wa sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, sikukuu ya kuvuna majuma na wakati wa sikukuu ya vibanda. Wasiende mbele ya Mwenyezi-Mungu mikono mitupu. Wote watatoa kadiri wanavyoweza kulingana na baraka Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alizowajalia. “Mtateua waamuzi na maofisa kutoka makabila yenu katika miji yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa, nao watatoa hukumu za haki kwa watu. Msipotoshe haki; msiwe na upendeleo, wala msikubali kupokea rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya watu wenye hekima na kupotosha kesi ya mtu mwadilifu. Mtazingatia haki tu, ili mpate kuishi na kuimiliki nchi mnayopewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Msipande mti wowote uwe nguzo ya mungu wa uongo karibu na meza ya madhabahu sadaka mtakayomjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Wala msisimamishe nguzo ambayo Mwenyezi-Mungu Mungu wako anaichukia. “Msimtolee Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, sadaka ya ng'ombe au kondoo mwenye dosari, wala ubaya wowote, maana hilo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Kama mkisikia kwamba katika mmoja wa miji yenu kuna mwanamume au mwanamke atendaye maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuvunja agano lake, naye amekwenda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, akaabudu hata jua, mwezi au vitu vingine vya mbinguni ambavyo sikuagiza viabudiwe, nanyi mkaambiwa hayo na mkaisikia taarifa hiyo, mtafanya uchunguzi kamili, na kama ni kweli na ni hakika kuwa kitu hiki kiovu kimefanywa katika Israeli, basi, mtoeni mtu huyo nje ya miji na kumpiga mawe mpaka afe. Hata hivyo, atauawa ikiwa kuna ushahidi wa watu wawili au watatu. Asiuawe ikiwa kuna ushahidi wa mtu mmoja tu. Wale mashahidi ndio watakaoanza kumpiga mawe kwanza, halafu wengine nao wampige mawe. Ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu. Inawezekana kukatokea mashtaka mengine yaliyo magumu mijini mwenu, kama vile kesi zihusuzo: Unajisi, mambo ya haki za watu, na madhara ya mwili. Ikitokea hivyo, mtaondoka na kwenda mahali alipopachagua Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na huko mtawaendea makuhani Walawi, na mwamuzi aliye kazini wakati huo, nanyi mtatoa mashtaka mbele yao, nao watatoa uamuzi wao. Kisha mtafanya kama watakavyowatangazieni pale mahali Bwana atakapopachagua; mtakuwa waangalifu kufanya yote kama watakavyowaagiza. Itawabidi kufanya kufuatana na maongozi watakayowapatia na uamuzi watakaoutoa kwenu. Msiache kutimiza kwa dhati hukumu watakayowatangazia. Naye mtu asiyejali kumtii kuhani au mwamuzi aliyewekwa hapo kumhudumia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, au mwamuzi, mtu huyo atauawa. Ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu. Watu wote watasikia na kuogopa wasifanye tena kitu kwa kutojali. “Mtakapokwisha ingia katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni, mkaimiliki na kukaa humo, nanyi mkasema, ‘Tutaweka mfalme juu yetu, kama mataifa yote yanayotuzunguka;’ mwaweza kumweka mfalme juu yenu mtu ambaye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atamchagua. Mtamweka mmojawapo wa ndugu zenu kuwa mfalme juu yenu. Msimfanye mgeni asiye ndugu yenu kuwa mfalme wenu. Hata hivyo, asiwe na farasi wengi kwa ajili yake mwenyewe, wala asiwarudishe watu Misri ili kujipatia farasi zaidi, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amewaonya, ‘Kamwe msirudi huko tena’. Wala asijipatie wake wengi, la sivyo moyo wake utaasi; wala asijipatie fedha na dhahabu kwa wingi mno. Atakapokuwa amekalia kiti cha ufalme lazima afanye nakala ya sheria hii iandikwe mbele ya makuhani wa Kilawi. Nakala hiyo atakuwa nayo daima na kuisoma maisha yake yote, ili apate kujifunza kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akishika na kutimiza maneno yote ya sheria hii na masharti haya, bila kujikuza mwenyewe juu ya ndugu zake, wala kuiweka kando amri hii kwa namna yoyote, ili aweze kudumu katika utawala, yeye na wazawa wake katika Israeli. “Makuhani Walawi, yaani kabila lote la Lawi wasiwe na sehemu wala urithi katika Israeli. Wao watakula sehemu ya sadaka za Mwenyezi-Mungu. Wala wasiwe na urithi kati ya ndugu zao; Mwenyezi-Mungu ndiye urithi wao kama alivyoahidi. “Na hii itakuwa haki ya makuhani kutoka kwa watu wanaotoa sadaka iwe ni ng'ombe au kondoo: Watampa kuhani mguu wa mbele, mashavu na matumbo. Mtawapa sehemu ya kwanza ya mazao yenu ya nafaka, divai, mafuta yenu na sufu ya kwanza ya kondoo wenu. Katika makabila yenu yote, Mwenyezi-Mungu amechagua kabila la Walawi limtumikie kama makuhani milele. “Ikiwa Mlawi yeyote atapenda mwenyewe anaweza kutoka mji wowote ule wa Israeli kwenda pale mahali Mwenyezi-Mungu alipochagua, na hapo anaweza kuhudumu kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama wale Walawi wengine wanaohudumu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Watapata mafungu yao sawa ya kula, ingawa wanayo mapato kutokana na mauzo ya mali za jamaa zao. “Mtakapofika katika ile nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawapa, msifuate desturi za kuchukiza za mataifa hayo. Pasiwe mtu yeyote miongoni mwenu atakayemtambika mtoto wake wa kiume au wa kike kwa moto, wala mtu apigaye ramli, wala mwaguzi, wala mpiga bao, wala mchawi, wala mlozi, wala mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo au kutoka kwa wafu. Maana yeyote atendaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; na kwa ajili ya mambo haya ya kuchukiza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawafukuza watu wa namna hiyo mbele yenu. Muwe wakamilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Mataifa haya ambayo mtaimiliki nchi yao hufuata maongozi ya waaguzi na wapiga ramli; lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu hawaruhusu nyinyi kufanya hivyo. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawateulieni nabii aliye kama mimi kutoka miongoni mwenu, nanyi mtamsikiliza huyo. Hicho ndicho mlichomwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kule Horebu, siku ile mlipokusanyika na kusema, ‘Tusisikie tena sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala tusiuone tena moto huu mkubwa, tusije tukafa!’ Naye Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Wamesema ukweli. Nitawateulia miongoni mwa ndugu zao wenyewe nabii kama wewe; nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. Yeyote ambaye hatasikia maneno atakayosema nabii huyo kwa jina langu, mimi mwenyewe nitamwadhibu. Lakini nabii yeyote atakayesema kwa jina la miungu mingine, au atakayejaribu kusema neno kwa jina langu hali mimi sikumwambia aseme, huyo nabii atakufa.’ “Lakini nyinyi mwaweza kusema, ‘Tutawezaje kutambua neno ambalo Mwenyezi-Mungu hakulisema?’ Kama nabii akisema kitu ati kwa jina la Mwenyezi-Mungu, na kitu hicho hakifanyiki au hakiwi kweli, jambo hilo hakulisema Mwenyezi-Mungu; nabii amelisema kwa ufidhuli, nanyi msitishwe na jambo hilo. “Baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuwaangamiza watu wale ambao nchi yao anawapeni, na baada ya kuimiliki na kuishi katika nyumba zao, mtatenga miji mitatu katika nchi atakayowapatia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, muimiliki. Mtatengeneza barabara na kugawa katika sehemu tatu nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapatia muimiliki ili kila anayemuua mtu bila kukusudia apate kukimbilia huko. “Mtu akimuua mwenzake bila kukusudia, naye hakuwa adui yake, anaweza kukimbilia mmojawapo wa miji hii, akayaokoa maisha yake. Kwa mfano, mtu aendaye na mwenzake msituni kukata kuni naye wakati anakata mti, shoka likachomoka kutoka kwenye mpini wake, likamuua yule mwingine, mtu huyo anaweza kukimbilia kwenye mji mmojawapo, akayaokoa maisha yake. Lakini kama umbali wa mji huo ni mkubwa mno, huyo mwenye kulipiza kisasi, kwa hasira kali anaweza kumfuatia, akamkamata na kumuua huyo aliyesababisha kifo, ingawaje hakupewa hukumu ya kifo na hao wahusika wawili hawakuwa maadui hapo awali! Kwa hiyo mimi nawaamuru mtenge miji mitatu. “Tena kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ataipanua mipaka ya nchi yenu, kama alivyowaapia babu zenu, naye akawapatia nchi yote ambayo aliahidi kuwapatia hao babu zenu ikiwa mtakuwa waangalifu kushika amri hizi zote ninazowaamuru hivi leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kufuata siku zote njia zake — basi, mtaongeza miji mingine mitatu zaidi ya hii mitatu, ili mtu asiye na hatia asije akauawa katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapatia kuwa yenu, na hivyo kuwasababisha kuwa na hatia ya mauaji. “Lakini mtu akiwa adui wa mwenzake, akamvizia akamshambulia na kumuua, kisha akakimbilia kwenye mji mmojawapo wa miji hiyo, hapo wazee wa mji huo watatuma watu wamtoe huko na kumkabidhi kwa mwenye kulipiza kisasi cha umwagaji damu, auawe. Msimwonee huruma, bali mtaukomesha uovu wa mauaji ya mtu asiye na hatia katika Israeli, ili mpate kuishi kwa amani. “Msiondoe alama ya mipaka ya jirani zenu, ambayo iliwekwa hapo zamani katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu wenu anawapatieni mwimiliki. “Ushahidi wa mtu mmoja hautoshi kumhukumu mtu juu ya kosa lolote la jinai au uovu kuhusu kosa lolote alilofanya. Ni ushahidi wa watu wawili au watatu tu ndio utakaothaminiwa. Ikiwa shahidi mdhalimu atatokea kumshtaki mtu yeyote juu ya kosa fulani, basi yeye na mshtakiwa kuhusu mzozo huo watakwenda mbele ya Mwenyezi-Mungu, mbele ya makuhani na waamuzi ambao wako katika ofisi wakati huo; waamuzi watachungua kwa uangalifu kesi hiyo na ikiwa mshahidi ni mshahidi wa uongo na amemshtaki mwenzake kwa uongo, basi, mtamtendea alivyokusudia kumtendea ndugu yake. Ndivyo mtakavyokomesha uovu kati yenu. Nao watu wengineo watasikia na kuogopa, na uovu kama huo hautafanyika tena kati yenu. Msiwaonee huruma watu wa aina hiyo. Uhai utalipwa kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono na mguu kwa mguu. “Mkienda vitani kupigana na adui zenu, mkaona farasi, magari na jeshi kubwa zaidi kuliko lenu msiwaogope. Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliyewatoa Misri, atakuwa nanyi. Kabla ya kuanza mapigano, kuhani atajitokeza mbele na kuwaambia watu, ‘Watu wa Israeli sikilizeni! Leo mnakaribia kupigana dhidi ya adui zenu. Msife moyo, au kuogopa, au kutishika, au kuwaogopa adui; maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye atakayekwenda pamoja nanyi kupigana kwa niaba yenu dhidi ya adui zenu na kuwapa ushindi.’ “Kisha maofisa watawaambia watu: ‘Kuna mtu yeyote hapa aliyejenga nyumba mpya lakini hajaizindua? Arudi nyumbani, asije akafia vitani na mtu mwingine akaizindua. Kuna mtu yeyote hapa aliyepanda mizabibu na ambaye hajafurahia matunda yake ya kwanza? Arudi nyumbani asije akafia vitani na mtu mwingine akafurahia matunda yake. Kuna mwanamume yeyote hapa aliyeposa na yuko karibu kuoa? Arudi nyumbani, asije akafia vitani, na mwanamume mwingine akaoa mchumba wake.’ Maofisa wataendelea kuwaambia watu, ‘Je, yupo hapa mtu aliyekufa moyo? Arudi nyumbani, asije akasababisha wenzake kufa moyo kama yeye.’ Maofisa wakisha sema na watu, basi makamanda watawaongoza watu. “Mnapokaribia mji kuushambulia, kwanza wapeni wakazi wake masharti ya amani. Wakazi wa mji huo wakitaka amani na kujisalimisha kwenu, basi watu wote waliomo humo watawatumikieni na kufanya kazi za kulazimishwa. Lakini wakazi wa mji huo wasipofanya amani nanyi, lakini wakapigana vita nanyi, basi, mtauzingira mji wao; naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu akiutia mikononi mwenu, mtawaua kwa upanga wanaume wote; lakini wanawake na watoto, ng'ombe, na vyote vilivyomo mjini, nyara zake zote mwaweza kuchukua mateka kwa ajili yenu wenyewe; mnaweza kufurahia nyara za adui zenu, ambazo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapa. Ndivyo mtakavyoitendea miji yote ambayo iko mbali na nchi mtakayoimiliki. Lakini katika miji ya nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni, msisalimishe chochote. Mtawaangamiza watu wote: Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyoamuru, wasije wakawafundisha desturi zao za kuchukiza ambazo waliifanyia miungu yao, nanyi mkatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Mkiuzingira mji kwa muda mrefu, mkapigana kuuteka, msiiharibu miti ya matunda kwa mashoka. Je, miti ni watu hata muishambulie? Mnaweza kula matunda ya miti hiyo, lakini msiikate. Mnaweza kukata tu miti mingine kuitumia kuuzingira mji mpaka muuteke. “Mtu akipatikana ameuawa mbugani katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni muimiliki, nanyi hamjui ni nani aliyemuua, wazee na waamuzi wenu watajitokeza na kupima umbali wa kutoka mahali maiti ilipo hadi miji ya karibu. Kisha, wazee wa mji ule ulio karibu zaidi na ile maiti watachukua ndama ambaye hajatumiwa kufanya kazi yoyote ile wala kutiwa nira. Nao watamteremsha ndama bondeni kwenye kijito ambacho hakikauki, na bonde hilo halilimwi au kupandwa; huko watamvunja huyo ndama shingo. Nao makuhani wa ukoo wa Lawi sharti wawepo hapo. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwachagua wamhudumie na kubariki watu kwa jina lake. Wao pia ndio wenye mamlaka kuhusu kila tukio na utumiaji wa nguvu. Yule ndama atakapovunjwa shingo, wazee wote wa mji huo ulio karibu na mtu huyo aliyeuawa, watanawa mikono yao kwa maji juu ya ndama na kusema, ‘Hatuna hatia kuhusu kifo hiki, wala hatumjui aliyemuua. Ee Mwenyezi-Mungu, uwasamehe watu wako wa Israeli ambao umewakomboa, usiwawekee watu wako Israeli hatia ya mauaji ya mtu asiye na hatia, ila uwasamehe hatia hiyo.’ Hivyo damu hiyo iliyomwagwa haitakuwa tena sababu ya lawama kwenu, maana mmefanya yale Mwenyezi-Mungu aliyotaka myafanye. “Mkienda kupigana vita na adui, naye Mwenyezi-Mungu akawapeni ushindi, mkawachukua mateka, kama mmoja wenu akiona miongoni mwa mateka mwanamke mzuri, akamtamani na kutaka kumwoa, basi, wewe mwanamume mhusika utamchukua nyumbani kwako, naye atanyoa kichwa chake, akakate kucha zake, na kubadili nguo zake za mateka. Atakaa muda wa mwezi mzima kumwombolezea baba yake na mama yake; kisha waweza kumwoa uwe mume wake, naye awe mke wako. Kama baadaye hupendezwi naye, utamwacha huru aende zake; usimwuze kwa fedha, wala usimfanye kama mtumwa, kwa sababu ulimnyenyekesha. “Ikiwa mwanamume fulani ana wake wawili naye anampenda mmoja kuliko mwingine. Nao wanawake hao wamemzalia watoto wa kiume, na mtoto wa kwanza kuzaliwa ni wa yule mama asiyempenda, ikafika siku ya kuwapa hao wanawe urithi, huyo baba haruhusiwi kamwe kumtendea mtoto wa yule mke anayempenda kama kwamba ni mtoto mzaliwa wa kwanza, badala ya yule mtoto wa mama asiyependwa ambaye ndiye aliye mzaliwa wa kwanza. Lazima amkubali yule mzaliwa wa kwanza, mtoto wa yule mwanamke asiyependwa, na kumpa haki yake: Sehemu ya mali zake mara mbili. “Kama mtu ana mtoto mkaidi na mtundu, asiyemtii baba yake au mama yake wanapompa nidhamu, basi, mama na baba yake huyo mtoto watamchukua mlangoni mwa nyumba anamoishi na kumpeleka kwa wazee katika lango la mji. Wazazi hao watawaambia wazee wa mji: ‘Mtoto wetu ni mkaidi na mtundu, hataki kutusikiliza, ni mlafi na mlevi.’ Hapo watu wa mji huo watampiga mawe mtoto huyo mpaka afe. Ndivyo mtakavyokomesha ubaya huo miongoni mwenu. Kila mtu katika Israeli atasikia tukio hilo na kuogopa. “Kama mtu amefanya kosa la jinai linalompasa auawe na akauawa kwa kutundikwa mtini, maiti yake isiachwe mtini usiku wote, bali mtaizika siku hiyohiyo. Maana mtu aliyenyongwa amelaaniwa na Mungu nanyi hamtaitia najisi nchi yenu mliyopewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, iwe mali yenu. “Ukimwona ng'ombe au kondoo wa ndugu yako amepotea, usimwache, bali mrudishe kwa ndugu yako. Lakini kama nyumbani kwa huyu ndugu si karibu au kama humjui mwenyewe, basi, utamchukua mnyama huyo nyumbani kwako, akae kwako mpaka mwenyewe atakapokuja, nawe umrudishie. Utafanya vivyo hivyo kuhusu punda au vazi au kitu chochote ambacho nduguyo amekipoteza. Kamwe usiache kumsaidia. “Ukiona punda au ng'ombe wa nduguyo ameanguka njiani, usiache kumsaidia nduguyo; utamsaidia kumwinua. “Wanawake wasivae nguo za wanaume, na wanaume wasivae nguo za wanawake. Anayefanya hivyo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Ukikuta kiota cha ndege mtini au njiani, kina makinda au mayai na mamandege ameyafunika hayo makinda au mayai, usimchukue mamandege na makinda yake. Utamwacha mamandege aende zake, lakini unaweza kuchukua makinda. Ukifanya hivyo utafanikiwa na kuishi maisha marefu. “Unapojenga nyumba, jenga ukingo pembeni mwa paa, usije ukalaumiwa kama mtu akianguka kutoka huko, akafa. “Usipande mizabibu yako pamoja na mimea mingine, la sivyo mazao yote yatakuwa haramu, siyo tu yale uliyopanda bali pia matunda ya mizabibu. “Usilime shamba kwa kutumia ng'ombe na punda pamoja. “Usivae mavazi yaliyofumwa kwa sufu na kitani. “Funga vishada katika pembe nne za vazi lako. “Mwanamume akioa mwanamke, halafu baadaye akate shauri kumwacha, na kumshtaki kwamba ametenda mambo ya aibu, na kumharibia sifa kwa kusema kwamba hakupata ushahidi wa ubikira wakati alipomwoa, basi, wazazi wa mwanamke huyo watachukua ushahidi wa ubikira wa binti yao kwa wazee kwenye lango la mji na kuwaambia, ‘Tulimwoza binti yetu kwa mtu huyu, lakini sasa hamtaki tena, na ajabu ni kwamba amemshtaki mambo ya aibu na kusema ati hakumkuta na ushahidi wowote wa ubikira. Hata hivyo ushahidi wa ubikira wa binti yetu ni huu.’ Halafu atakunjua nguo yenye huo ushahidi mbele ya wazee wa mji. Hapo wazee wa mji watamchukua yule mwanamume na kumpiga viboko. Pia watamtoza mtu huyo faini ya vipande 100 vya fedha na kupewa baba wa huyo mwanamke kwa kuwa mwanamume huyo amemharibia sifa binti wa Israeli. Na huyo mwanamke ataendelea kuwa mke wake na hataweza kumpa talaka maisha yake yote. Lakini kama mashtaka hayo ni ya kweli, na hakuna ushahidi wa ubikira wake, watampeleka kwenye mlango wa nyumba ya baba yake na wanaume wa mji huo watampiga mawe afe, kwa sababu amefanya ufidhuli katika Israeli kwa kufanya umalaya akiwa nyumbani kwa baba yake. Ndivyo mtakavyokomesha uovu huo miongoni mwenu. “Mwanamume akifumaniwa na mke wa mtu mwingine, wote wawili, mwanamume na mwanamke, lazima wauawe. Ndivyo mtakavyokomesha uovu huo miongoni mwenu. “Mwanamume akimkuta msichana aliyechumbiwa, akalala naye, mtawatoa wote wawili nje ya mji na kuwapiga mawe mpaka wafe. Msichana huyo lazima auawe kwa kuwa hakupiga kelele asaidiwe ingawa alikuwa mjini; naye mwanamume lazima auawe kwa kuwa amemchafua mchumba wa jirani yake. Ndivyo mtakavyokomesha uovu huo miongoni mwenu. “Lakini kama mwanamume amekutana na msichana aliyechumbiwa akamshika kwa nguvu, basi ni huyo mwanamume tu atakayeuawa. Msimtendee huyo msichana chochote; yeye hana kosa linalostahili adhabu ya kifo. Tukio hili ni sawa na la mtu anayemshambulia mtu mwingine na kumwua, kwa sababu mwanamume huyo alimshika kwa nguvu huyo msichana huko mbugani, na ingawa alipiga kelele kuomba msaada hapakuwa na mtu wa kumsaidia. “Mwanamume akikutana na msichana ambaye hajachumbiwa, akamshika kwa nguvu, wakafumaniwa, mwanamume huyo atamlipa baba yake msichana huyo vipande hamsini vya fedha kwa sababu amemnajisi, na msichana huyo atakuwa mke wake, wala hana ruhusa ya kumwacha maisha yake yote. “Mwanamume yeyote kamwe asilale na mke wa baba yake. “Mwanamume yeyote aliyehasiwa au aliyekatwa uume wake haruhusiwi kujiunga na kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu. “Na mwana haramu yeyote, wala mzawa wake hata kizazi cha kumi, haruhusiwi kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu. “Mwamoni au Mmoabu yeyote, wazawa wao wote hata kizazi cha kumi, hawaruhusiwi kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu, kwa sababu walikataa kuwapatia chakula na maji mlipokuwa njiani kutoka Misri, na kwa kuwa walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori kule Mesopotamia, awalaani. Lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, hakumsikiliza Balaamu; badala yake laana hiyo iligeuka kuwa baraka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwapenda. Kwa hiyo, kamwe msiwasaidie hao wapate amani na fanaka. “Msiwachukie Waedomu; hao ni ndugu zenu. Na msiwachukie Wamisri, kwani mlikaa katika nchi yao kama wageni. Wazawa wao, kuanzia kizazi cha tatu, wataruhusiwa kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu. “Mkienda vitani, mkapiga kambi, kila mmoja ajihadhari na kitu chochote kiovu. Kama miongoni mwenu kuna mtu yeyote ambaye ni najisi kwa sababu ya kutokwa mbegu usiku, huyo atatoka nje ya kambi; hatakaa karibu na kambi. Lakini ikifika jioni ataoga, na jua likitua anaweza kurudi kambini. “Lazima muwe na mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda haja. Kati ya vifaa vyenu mtakuwa na jembe, na hilo mtatumia kuchimba shimo na kufukia kinyesi chenu. Kambi yenu lazima iwe takatifu kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anatembea kambini mwenu ili awaokoe na kuwatia adui zenu mikononi mwenu. Kwa hiyo msimwache aone kitu chochote kisichofaa miongoni mwenu, la sivyo atawaacheni. “Mtumwa akikimbilia kwako usimrudishe kwa bwana wake. Ataishi pamoja nawe mahali atakapochagua katika mojawapo ya makao yako, mahali panapompendeza. Usimdhulumu. “Mwisraeli yeyote, mwanamume au mwanamke, haruhusiwi kamwe kuwa kahaba wa kidini. Fedha yoyote iliyopatikana kwa vitendo vya ukahaba huo, isipelekwe hekaluni kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kulipia nadhiri, maana mwanamume au mwanamke aliye kahaba wa kidini ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu. “Usimkopeshe ndugu yako Mwisraeli kitu kwa riba; usimtoze riba juu ya mkopo wa fedha, chakula, au chochote ambacho watu hukopesha kwa riba. Unaweza kutoza riba unapomkopesha mgeni, lakini ndugu yako Mwisraeli usimtoze riba, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atakubariki katika shughuli zako zote utakazofanya katika nchi ambayo unakwenda kuimiliki. Unapoweka nadhiri kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, usichelewe kuitekeleza, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wako ataidai kwako, nawe utakuwa na kosa. Lakini ukiacha kuweka nadhiri hutakuwa na dhambi. Uwe mwangalifu kutimiza nadhiri uliyotamka kwa mdomo wako, maana ulimwahidi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, kwa hiari yako. “Ukipitia katika shamba la mzabibu la jirani yako unaweza kula zabibu kadiri uwezavyo, lakini usichume na kuchukua zabibu zozote kikapuni mwako. Ukipitia katika shamba la jirani yako lenye nafaka unaweza kukwanyua masuke kwa mkono na kula, lakini usichukue mundu kukata mazao yake. “Ikiwa mwanamume ameoa mke na baadaye akawa hapendezwi naye kwa sababu ameona kwake kitu kisichofaa, basi, huyo mwanamume akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza nyumbani mwake, kisha huyo mwanamke akaondoka, akaolewa na mwanamume mwingine, kama huyo mume wa pili akimchukua, akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza nyumbani mwake, au kama huyo mumewe akifa, basi, yule mume wa kwanza haruhusiwi tena kumchukua huyo mwanamke kuwa mke wake kwa sababu alikwisha kutiwa unajisi. Kufanya hivyo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu. “Mwanamume aliyeoa karibuni asiende vitani wala asipewe kazi yoyote nyingine; aachwe huru kwa muda wa mwaka mmoja, ili akae nyumbani na kufurahi na mkewe. “Mtu yeyote asichukue jiwe la chini au la juu la kusagia kuwa rehani; kufanya hivyo ni kama kuchukua uhai wa mtu huyo. “Mtu yeyote akimwiba Mwisraeli mwenzake na kumfanya mtumwa wake au kumwuza utumwani, mtu huyo lazima auawe. Ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu. “Kama mtu akishikwa na ukoma mnapaswa kuwa waangalifu kufuata maagizo ya Walawi. Kama nilivyowaamuru ndivyo mtakavyofuata kwa uangalifu. Kumbukeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu alivyomtendea Miriamu mlipokuwa safarini kutoka Misri. “Ukimkopesha jirani kitu chochote, usiingie kwake kuchukua rehani. Msubiri nje na umwache yeye mwenyewe akuletee hiyo rehani. Kama yeye ni maskini usikae na rehani hiyo usiku kucha. Mrudishie kila siku jioni ili usiku aweze kujifunika na kukutakia baraka. Kufanya hivyo ni jambo la uadilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Usimdhulumu kibarua maskini na mhitaji, awe Mwisraeli au mmoja wa wageni wanaoishi katika miji yenu. Kila siku, kabla jua halijakuchwa, mlipe ujira wake wa siku hiyo, maana yeye ni maskini na huo ujira ni tegemeo la moyo wake; ili asije akamlilia Mwenyezi-Mungu, nawe ukawa na hatia. “Wazazi wasiuawe kwa makosa ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya makosa ya wazazi wao. Kila mtu atauawa kwa makosa yake mwenyewe. “Msipotoshe haki za wageni na yatima. Wala msichukue vazi la mjane kuwa rehani. Kumbukeni kwamba nyinyi mlikuwa watumwa nchini Misri, na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, akawakomboa kutoka huko. Kwa hiyo ninawapeni amri hiyo. “Mnapovuna mavuno yenu shambani na kusahau masuke mengine humo, msirudi kuyachukua, ila waachieni wageni, yatima na wajane, ili Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu awabariki katika kazi zenu zote. Mkipukutisha mizeituni yenu kuvuna matunda, msirudi kupukutisha tena vitawi vyake, ila waachieni wageni, yatima na wajane. Mnapochuma zabibu, msirudi kuokota zabibu zilizobaki ila waachieni wageni, yatima na wajane. Mtakumbuka kuwa nyinyi mlikuwa watumwa nchini Misri; kwa hiyo ninawapeni amri hii. “Ikiwa kuna ugomvi kati ya watu wawili, wakaenda kuamuliwa mahakamani, mmoja akaonekana hana hatia, na mwingine akahukumiwa, kama yule aliyehukumiwa amepewa adhabu ya kuchapwa viboko, hakimu atamwamuru huyo alale chini na kuchapwa viboko kulingana na kosa lake. Mwenye hatia anaweza kuchapwa viboko arubaini lakini si zaidi. Mkizidisha kiasi hicho mtakuwa mmemfedhehesha ndugu yenu. “Usimfunge ng'ombe kinywa anapopura nafaka. “Kama ndugu wawili wa kiume wanaishi mahali fulani na mmoja wao akafariki bila kuacha mtoto wa kiume, mkewe marehemu asiolewe na mtu mwingine nje ya jamaa hiyo. Ni wajibu wa ndugu wa marehemu kumwoa mjane huyo. Mtoto wa kwanza wa kiume atakayezaliwa nao atahesabiwa kuwa mtoto wa marehemu, ili jina lake lisifutwe nchini Israeli. Lakini kama huyo ndugu wa marehemu hamtaki huyo mwanamke mjane, basi, mwanamke huyo atakwenda mbele ya wazee wa mji na kusema, ‘Kaka wa mume wangu marehemu anakataa kuendeleza jina la kaka yake marehemu katika Israeli; hapendi kunitimizia jukumu lake la kaka wa mume wangu marehemu.’ Kisha wazee wa mji watamwita huyo mwanamume kuongea naye. Kama bado atasisitiza kwamba hataki kumwoa, huyo mwanamke mjane atamwendea mbele ya hao wazee wa mji, atamvua kiatu chake kimoja na kumtemea mate usoni na kumwambia, ‘Hivi ndivyo anavyopaswa kutendewa mtu anayekataa kuidumisha nyumba ya kaka yake.’ Na jina la nyumba yake katika Israeli litakuwa: ‘Nyumba ya mtu aliyevuliwa kiatu.’” “Wanaume wawili wakipigana na mke wa mmoja wao akamsaidia mumewe kwa kumkamata sehemu za siri yule anayepigana na mumewe, mtaukata mkono wa kulia wa huyo mwanamke; msimhurumie. “Msiwe na vipimo vya kupimia vya namna mbili: Kimoja kizito na kingine chepesi. Msitumie mizani za udanganyifu. Wala msiwe na aina mbili za vipimo vya kupimia, kubwa na ndogo. “Tumieni mizani na vipimo vyenye uzito sahihi ili mpate kuishi maisha marefu katika nchi anayowapa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Wote wanaofanya mambo hayo, wote wanaotenda kwa udanganyifu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Kumbukeni kitendo cha Waamaleki mlipokuwa safarini kutoka Misri. Kumbukeni walivyowashambulieni huko njiani mkiwa wanyonge na kuwapiga wale wote waliokuja nyuma yenu wamechoka. Waamaleki hawakumwogopa Mungu. Kwa hiyo wakati Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapowapumzisha kutokana na mashambulio ya adui zenu wote wanaowazunguka katika nchi ambayo amewapa mwimiliki na kuishi humo, ni lazima muwaangamize Waamaleki wote. “Baada ya kufika na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapa iwe yenu na kuishi huko, baadhi ya malimbuko ya mazao utakayovuna katika nchi anayokupa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, utayachukua katika kikapu mpaka pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amepachagua pawe makao yake. Utamwendea kuhani anayehudumu wakati huo, na kumwambia, ‘Leo ninakiri mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kuwa nimeingia katika nchi aliyowaapia wazee wetu kuwa atatupa.’ “Naye kuhani atakapochukua kikapu hicho mikononi mwako na kukiweka mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, utatamka maneno haya mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako: ‘Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyetangatanga huko na huko, kisha akashuka kwenda Misri akaishi huko kama mgeni. Yeye na jamaa yake walikuwa watu wachache tu walipokuwa huko, lakini wakawa taifa kubwa lenye nguvu na watu wengi. Wamisri walitutendea kwa ukatili wakatutesa na kutulazimisha kufanya kazi ngumu ya watumwa. Kisha tukamlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wetu, akasikia kilio chetu, na kuyaona mateso yetu, kazi ngumu na dhuluma tulizozipata. Basi, Mwenyezi-Mungu akatutoa huko Misri kwa mkono wake wa nguvu ulionyoshwa, kwa vitisho, ishara na maajabu. Alituleta hapa na kutupatia nchi hii inayotiririka maziwa na asali. Na sasa ninamletea Mwenyezi-Mungu malimbuko ya mazao ya nchi ambayo amenipa.’ “Kisha utaweka kikapu chini, mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na kuabudu mbele zake. Nawe utafurahia mema yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amekujalia wewe na jamaa yako. Nao watafurahi pamoja nawe. Kila baada ya miaka mitatu, kila mmoja wenu atatoa sehemu moja ya kumi ya mazao yake yote kwa ajili ya Walawi na wageni, yatima na wajane, ili wapate chakula chote wanachohitaji wanapokuwa katika miji yenu. Kisha utasema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, hivi: ‘Nimelitoa nyumbani kwangu fungu takatifu, nikawapa Walawi, wageni, yatima na wajane, kama ulivyoniamuru nifanye. Sijavunja amri zako wala sijasahau. Sikula zaka yoyote nilipokuwa ninaomboleza; sikuitoa nje ya nyumba yangu nilipokuwa najisi na sikutoa zaka hiyo kwa wafu. Nimekutii ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoamuru. Uangalie chini kutoka makao yako matakatifu mbinguni, uwabariki watu wako Israeli na nchi uliyotupatia kama ulivyowaapia wazee wetu; nchi inayotiririka maziwa na asali.’ “Leo hii, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawaamuru kuyashika masharti na maagizo haya. Muwe waangalifu kuyatekeleza kwa moyo wote na roho yote. Leo hii mmekiri Mwenyezi-Mungu, kuwa Mungu wenu, na kwamba mtafuata njia zake na kushika masharti, amri zake na maagizo yake na kutii sauti yake. Naye Mwenyezi-Mungu ametamka rasmi leo hii kwamba nyinyi ni watu wake yeye mwenyewe kama alivyowaahidi na kwamba mnatakiwa kushika amri zake zote. Atawafanyieni nyinyi kuwa taifa kubwa kuliko mataifa yote aliyoyaumba. Nanyi mtalitetea jina lake, sifa yake na heshima yake. Nyinyi mtakuwa watu wake, walio mali yake, kama alivyoahidi.” Basi, Mose akiwa pamoja na wazee wa Israeli aliwaambia watu hivi: “Shikeni amri zote ninazowapa leo. Siku ile mtakapovuka mto Yordani na kuingia katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni, mtasimika mawe makubwa na kuyapiga lipu. Juu yake mtaandika maneno yote ya sheria zote hizi, mtakapoingia katika nchi inayotiririka maziwa na asali ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wenu, aliwaahidi. Mkiwa ngambo ya mto Yordani, mtasimika mawe hata juu ya mlima Ebali, kama ninavyowaamuru hivi leo, na kuyapiga lipu. Mtamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, madhabahu mahali hapo palipo na mawe ambayo hayakuchongwa. Naam, madhabahu yoyote mtakayomjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, lazima ijengwe kwa mawe yasiyochongwa. Juu ya madhabahu hiyo mtamtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu sadaka za kuteketezwa. Mtamtolea sadaka za amani, na kula papo hapo na kufurahi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mtaandika waziwazi juu ya mawe hayo maneno yote ya sheria hii.” Basi, Mose pamoja na makuhani Walawi wakawaambia watu wote wa Israeli, “Nyamazeni mnisikilize enyi watu wa Israeli. Leo hii nyinyi mmekuwa watu wake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kwa hiyo mtatii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu mkizifuata amri zake na masharti yake ambayo ninawaamuru leo.” Siku hiyo Mose aliwaagiza watu na kusema, “Mkisha vuka Yordani, makabila yafuatayo yatasimama juu ya mlima Gerizimu kuwabariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yosefu na Benyamini. Na makabila yafuatayo yatasimama juu ya mlima Ebali wakati laana zitakapotolewa: Reubeni, Gadi, Asheri, Zebuluni, Dani na Naftali. Nao Walawi watawatangazia watu wote wa Israeli kwa sauti kubwa: “ ‘Alaaniwe mtu yeyote afanyaye sanamu ya kuchonga au ya kusubu na kuisimamisha kwa siri, kitu ambacho kimetengenezwa na mikono ya fundi na ambacho ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayemdharau baba yake au mama yake.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mtu yeyote aondoaye alama ya mpaka wa jirani yake.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mtu yeyote ampotoshaye kipofu njiani.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayepotosha haki ya mgeni au yatima au mjane’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mwanamume alalaye na mke wa baba yake, maana amemwaibisha baba yake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na mnyama yoyote’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na dada yake awe ni binti ya baba yake au binti ya mama yake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na mama mkwe wake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayeua mtu kwa siri’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mtu yeyote apokeaye hongo ili aue mtu asiye na hatia’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “ ‘Alaaniwe mtu yeyote asiyekubali maneno haya ya sheria na kuyatii’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’ “Kama mkiitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu na kuzingatia kwa uangalifu amri ambazo ninawaamuru leo, yeye atawaweka juu ya mataifa yote duniani. Kama mkitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mtapewa baraka zifuatazo; “Miji yenu itabarikiwa na mashamba yenu. “Mtabarikiwa mpate wazawa wengi, mavuno mengi, ng'ombe na kondoo wengi. “Vikapu vyenu vya nafaka vitabarikiwa na vyombo vyenu vya kukandia. Mtabarikiwa mnaporudi nyumbani na mnapotoka nje. Maadui zenu wakiwashambulia, Bwana atawapeni ushindi juu yao. Wakija kuwashambulia kwa njia moja watawakimbieni kwa njia saba. Baraka za Mwenyezi-Mungu zitakuwa katika ghala zenu za nafaka na katika shughuli zenu zote. Atawabariki katika nchi ambayo anawapeni. “Mwenyezi-Mungu atawafanyeni kuwa watu wake watakatifu kama alivyowaahidi, kama mkizitii amri zake yeye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kufuata njia zake. Mataifa yote duniani yakiona kwamba nyinyi mnaitwa kwa jina la Mwenyezi-Mungu yatawaogopa. Mwenyezi-Mungu atawafanikisha kwa wingi: Watoto, mifugo na mavuno shambani katika nchi aliyowaapia wazee wenu kuwa atawapeni, Mwenyezi-Mungu atawafungulieni hazina yake nzuri kutoka mbinguni na kunyesha mvua katika nchi kwa wakati wake, na kubariki kazi zenu. Mtayakopesha mataifa mengi, lakini nyinyi hamtakopa. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawafanya kuwa wa kwanza kwa nguvu na sio wa mwisho. Mtaendelea mbele na sio kurudi nyuma kama mkishika amri zake ambazo ninawapeni leo na kuwa waangalifu kuzitekeleza, bila kugeuka kulia au kushoto kuifuata miungu mingine na kuitumikia. “Lakini kama hamtaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, au msipokuwa waangalifu kutekeleza amri zake zote na masharti ninayowaamuru leo, basi mtapatwa na laana hizi zote: Mtapata laana katika miji yenu na mashamba yenu. Vikapu vyenu vya nafaka vitalaaniwa na vyombo vyenu vya kukandia mkate. Watoto wenu watalaaniwa na mazao yenu ya nchi; mifugo yenu italaaniwa isiongezeke. Mtalaaniwa mnapoingia na mnapotoka. “Mwenyezi-Mungu atawaleteeni maafa, vurugu na kukata tamaa katika shughuli zenu zote mpaka mmeangamia upesi kwa sababu ya uovu wa matendo yenu na kwa sababu ya kumwacha Mwenyezi-Mungu. Atawaleteeni maradhi mabaya mpaka wote muangamie kabisa katika nchi ambayo mnaenda kuimiliki. Mwenyezi-Mungu atawashambulia kwa kifua kikuu, homa, majipu, joto kali, ukame, dhoruba na ukungu; mambo hayo yatawaandama mpaka mmeangamia. Mbingu zitakauka kama shaba nyeusi bila mvua, na nchi itakuwa kama chuma. Mwenyezi-Mungu ataifanya vumbi na mchanga kuwa mvua yenu, vumbi litawanyeshea mpaka mmeangamizwa. “Mwenyezi-Mungu atawafanya mshindwe na adui zenu. Nyinyi mtakwenda kuwakabili kwa njia moja, lakini mtawakimbia kwa njia saba. Nanyi mtakuwa kinyaa kwa watu wote duniani. Maiti zenu zitakuwa chakula cha ndege wala hapatakuwa na mtu atakayewafukuza. Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa majipu yaliyowapata Wamisri, atawapeni vidonda, upele na kuwashwa ambavyo hamwezi kuponywa. Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa pigo la kuwa na wazimu, mtakuwa vipofu na kuvurugika akili. Mtakwenda kwa kupapasapapasa mchana kama vipofu wala hamtafanikiwa katika shughuli zenu. Mtakuwa mkidhulumiwa kila mara na hakutakuwa na mtu wa kuwasaidieni. “Mtachumbia wasichana lakini watu wengine watalala nao. Mkijenga nyumba watu wengine watakaa ndani yake. Mkipanda mizabibu watu wengine watavuna. Ngombe wenu watachinjwa mbele ya macho yenu lakini hamtaonja hata kipande cha nyama yao. Punda wenu watachukuliwa kwa nguvu mbele ya macho yenu wala hamtarudishiwa. Kondoo wenu watapewa adui zenu, na hakuna mtu atakayeweza kuwasaidia. Watoto wenu wa kiume na wa kike watatolewa kwa watu wengine huku mkikodoa macho mchana kutwa kuwatazamia warudi, lakini hamtakuwa na nguvu ya kufanya chochote. “Taifa msilolijua litachukua mazao yote ya nchi yenu na matunda ya jasho lenu, nanyi mtadhulumiwa na kuteswa daima, hata mtapata wazimu kwa mambo mtakayoona kwa macho yenu wenyewe. Mwenyezi-Mungu atayashambulia magoti yenu na miguu yenu kwa majipu mabaya ambayo hamtaweza kuponywa; yatawaenea tangu utosini mpaka nyayo za miguu. “Mwenyezi-Mungu atawapeleka nyinyi na mfalme wenu mtakayejichagulia, mpaka kwa taifa ambalo nyinyi hamkulijua wala wazee wenu. Na huko mtatumikia miungu mingine ya miti na mawe. Nanyi mtakuwa kinyaa, dharau na mshangao miongoni mwa watu wote wa nchi ambako Mwenyezi-Mungu atawapeleka. Mtapanda mbegu nyingi lakini mtavuna kidogo tu kwa kuwa nzige watakula mazao yenu. Mtapanda mizabibu na kuitunza, lakini hamtavuna mizabibu hiyo wala kunywa divai yake, maana wadudu wataila. Mtakuwa na mizeituni mahali pote nchini mwenu, lakini hamtakuwa na mafuta ya kujipaka; kwa sababu zeituni hizo zitapukutika. Mtazaa watoto wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa wenu, watachukuliwa uhamishoni. Matunda yenu yote na mazao yenu mashambani vitamilikiwa na nzige. “Wageni waishio katika nchi yenu watazidi kupata nguvu huku nyinyi mkizidi kufifia zaidi na zaidi. Wao watawakopesha nyinyi, lakini nyinyi hamtakuwa na uwezo wa kuwakopesha. Wao watakuwa wa kwanza kwa nguvu nanyi mtakuwa wa mwisho. “Hayo yote yatawapateni nyinyi na kuwaandama mpaka muangamizwe kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kuhusu kushika amri zake na masharti aliyowapa. Lakini hizo zitakuwa ushahidi wa hukumu ya Mwenyezi-Mungu kwenu na wazawa wenu milele. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwabariki katika kila njia, lakini nyinyi hamkumtumikia kwa moyo wa furaha na mkunjufu. Kwa hiyo mtawatumikia maadui zenu ambao Mwenyezi-Mungu atawatuma dhidi yenu, kwa njaa, kiu na uchi, na kutindikiwa kila kitu. Atawafungeni nira ya chuma mpaka awaangamize. “Mwenyezi-Mungu ataleta kutoka mbali taifa moja liwavamie kasi kama tai, taifa ambalo lugha yake hamuielewi. Taifa hilo lenye watu wa nyuso katili halitajali wazee wala kuwahurumia vijana; litakula ng'ombe wenu na mazao yenu, mpaka mmeangamizwa. Halitawaachieni nafaka, divai, mafuta, ng'ombe au kondoo mpaka liwaangamize. Watu hao watawazingira katika miji yenu yote, mpaka kuta zenu za ngome ambazo mlitegemea zimeporomoshwa chini kila mahali katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni. Wakati wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui wenu, mtakula watoto wenu ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapeni. Hata mtu mpole kabisa na aliyelelewa vizuri sana atamnyima chakula ndugu yake, mkewe ampendaye na mtoto wake atakayesalia; wala hatamgawia hata mmoja wao nyama ya watoto wake atakaowala. Hamtabakiwa na chochote wakati huo wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui katika miji yenu yote. Hata mwanamke yule ambaye ni mpole sana na aliyelelewa vizuri na mwororo hata hajawahi kukanyaga udongo kwa kisigino chake hataweza kufanya vingine. Wakati huo wa kuzingirwa kutakuwa na njaa hata atamla mtoto wake mchanga na kile kinachotoka baada ya kuzaliwa mtoto bila hata mumewe mpenzi au mmoja wa watoto wake kutambua. “Kama msipokuwa waangalifu kutekeleza maneno yote ya sheria hii iliyoandikwa katika kitabu hiki na msipoliheshimu na kulitukuza jina tukufu la kuogofya la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, basi, Mwenyezi-Mungu atawaleteeni nyinyi na wazawa wenu mateso yasiyo ya kawaida, mateso makali yasiyoponyeka na ya kudumu, na magonjwa makali ya kudumu. Atawaleteeni tena yale magonjwa mliyoyaogopa nchini Misri, nayo yatawaandama daima. Atawaleteeni magonjwa ya kila aina na mateso mengine ambayo hayakutajwa katika kitabu hiki cha sheria mpaka muangamie. Ijapokuwa nyinyi ni wengi kama nyota za mbinguni, lakini mtakuwa wachache tu kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kama vile Mwenyezi-Mungu alivyopendezwa kuwafanikisha na kuwafanya kuwa wengi, vivyo hivyo Mwenyezi-Mungu atapendezwa kuwaletea maafa na kuwaangamiza. Nanyi mtaondolewa katika nchi hiyo ambayo mnakwenda kuimiliki. Mwenyezi-Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka pembe moja ya dunia hadi nyingine na huko mtaitumikia miungu mingine ya miti na mawe, miungu ambayo nyinyi wala wazee wenu hawakuijua. Hamtakuwa na raha yoyote mahali penu wenyewe pa kutulia wala miongoni mwa mataifa hayo. Ila Mwenyezi-Mungu atawapeni huko wasiwasi wa moyo, kufifia kwa macho na mahangaiko ya rohoni. “Maisha yenu yatakuwa mashakani, mchana na usiku mtakuwa na hofu na hamtakuwa na usalama wa maisha. Mioyo yenu itajaa woga wa kila mtakachoona. Asubuhi mtasema, ‘Laiti ingekuwa jioni,’ jioni itakapofika mtasema, ‘Laiti ingekuwa asubuhi.’ Mwenyezi-Mungu atawarudisheni Misri kwa meli, safari ambayo aliahidi kwamba hamngeifanya tena. Huko mtajaribu kujiuza kwa maadui zenu kuwa watumwa, lakini hakuna mtu atakayewanunua.” Haya ni maneno ya agano ambalo Mwenyezi-Mungu aliwaamuru Mose kufanya na Waisraeli katika nchi ya Moabu, licha ya agano Mwenyezi-Mungu alilofanya nao mlimani Horebu. Mose aliwaita pamoja Waisraeli wote akawaambia, “Mliona nyinyi wenyewe jinsi Mwenyezi-Mungu alivyomtendea mfalme wa Misri, maofisa, watumishi wake na nchi yake yote. Mliona maafa makubwa, ishara na maajabu aliyotenda. Lakini mpaka leo Mwenyezi-Mungu hajawapa akili ya kuelewa, macho ya kuona, wala masikio ya kusikia! “Kwa muda wa miaka arubaini, mimi niliwaongoza jangwani, nguo zenu mlizovaa hazikuchakaa wala viatu vyenu havikuchakaa miguuni mwenu. Hamkula mkate wala kunywa divai au kileo chochote kile, mpate kujua kwamba Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu. “Na mlipofika mahali hapa, mfalme Sihoni wa Heshboni na mfalme Ogu wa Bashani walikuja kupigana nasi; lakini tukawashinda, tukaichukua nchi yao, tukayagawia makabila ya Reubeni na Gadi na nusu kabila la Manase iwe mali yao. Kwa hiyo muwe waangalifu kushika maneno yote ya agano hili ili mpate kufanikiwa katika kazi zenu zote. “Leo, mmesimama mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi nyote viongozi wa makabila, wazee wenu, maofisa wenu, watoto wenu na wake zenu, wageni wanaoishi miongoni mwenu ambao hukata kuni na kuwatekea maji. Mko hapa leo ili kufanya agano hili ambalo Bwana Mungu wenu anafanya leo, kwamba atawathibitisha leo kuwa watu wake naye atakuwa Mungu wenu, kama alivyowaapia nyinyi na babu zenu: Abrahamu, Isaka na Yakobo. Wala sifanyi agano hili leo kwa niaba yenu tu na kutamka laana zake; sifanyi kwa niaba ya wale tu walio pamoja nasi leo mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, bali pia kwa niaba ya wale ambao hawapo pamoja nasi leo. “Mnajua jinsi tulivyoishi nchini Misri na jinsi tulivyosafiri katika nchi za mataifa mengine. Mliona sanamu zao za kuchukiza, miungu ya miti na mawe, ya fedha na dhahabu. Chukueni hadhari kwamba hakuna mwanamume, mwanamke, jamaa au kabila lolote linalosimama hapa leo litakalomwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwenda kutumikia miungu ya mataifa mengine. Jambo hili litakuwa kama mzizi utakaomea na kuzaa matunda machungu yenye sumu. Kama baada ya kusikia maneno ya agano hili ambayo mmeapishwa, halafu mtu akajiamini mwenyewe moyoni mwake na kusema atakuwa salama, hata kama atafuata ukaidi wake mwenyewe, hiyo itawaangamiza wote, wabaya na wema. Mwenyezi-Mungu hatasamehe mtu huyo, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu na wivu wake vitamwakia mtu huyo; laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamjia, naye Mwenyezi-Mungu atalifuta kabisa jina la mtu huyo kutoka duniani. Mwenyezi-Mungu atamtenga kutoka miongoni mwa makabila yote ya Israeli apatwe na maafa kufuatana na laana zote za agano zilizoandikwa katika kitabu hiki. Katika vizazi vijavyo, wazawa wenu na wageni kutoka nchi ya mbali wataona jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoiletea nchi hii maafa na mateso: Imejaa madini ya kiberiti na chumvi, imeteketea na kuwa tupu, haikupandwa mbegu na haioti chochote. Ni kama ilivyokuwa wakati Mwenyezi-Mungu alipoangamiza Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, kwa hasira yake kali. Naam, mataifa yote yatasema: ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ameitendea hivyo nchi hii? Hasira hii kubwa inamaanisha nini?’ Na jibu litatolewa: ‘Ni kwa sababu walivunja agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao ambalo alifanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri, wakaenda kuitumikia na kuiabudu miungu mingine, ambayo hawakuijua hapo awali, wala Mwenyezi-Mungu hakuwa amewapa. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya nchi hii, na kuiletea laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki. Naye Mwenyezi-Mungu, akawangoa kutoka katika nchi yao kwa hasira na ghadhabu kubwa, akawatupa katika nchi nyingine kama ilivyo leo.’ “Mambo ya siri ni ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, lakini yale ambayo ameyafunua ni yetu na wazawa wetu milele, ili tutekeleze maneno yote ya sheria hii.” Mose akaendelea kusema, “Nimewapeni uchaguzi kati ya baraka na laana. Mambo hayo yote yakiwapata nanyi mkiyatafakari popote mlipo miongoni mwa mataifa ambamo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atakuwa amewatawanya, mkamrudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi na watoto wenu, mkatii kwa moyo wote na roho yote neno lake ninalowaamuru leo, hapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawarudishieni mema yenu na kuwahurumia na kuwakusanya tena kutoka katika mataifa ambamo atakuwa amewatawanya. Na hata kama mmetawanywa katika sehemu mbali kabisa duniani, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawakusanya na kuwarudisheni, ili muimiliki tena nchi ambamo waliishi wazee wenu. Naye atawafanya mfanikiwe zaidi na kuwa wengi kuliko wazee wenu. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawafanyeni nyinyi na wazawa wenu muwe na moyo wa utii ili mumpende yeye kwa moyo wenu wote na roho yenu yote, mpate kuishi. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atazifanya laana hizi zote ziwapate adui zenu ambao waliwatesa. Nanyi mtaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu na kuzishika amri zake zote ninazowapeni leo. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawafanya mfanikiwe katika kila mtakalofanya; mtakuwa na watoto wengi na ng'ombe wengi na mashamba yenu yatatoa mazao. Maana atapenda tena kuwafanya mfanikiwe kama vile alivyopenda kuwafanikisha wazee wenu, ikiwa mtiatii sauti yake na kushika amri na masharti yake yaliyoandikwa katika kitabu hiki cha sheria na kumrudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa moyo wote na roho yote. “Amri ninazowapa leo si ngumu mno kwenu, wala haziko mbali nanyi. Haziko mbinguni hata mseme, ‘Nani atakayepanda juu mbinguni kutuletea ili tupate kuzisikia na kuzitii?’ Wala haziko ngambo ya bahari, hata mseme, ‘Nani atakayevuka bahari atuletee ili tuzisikie na kuzitii.’ Sivyo, ila zipo karibu nanyi, vinywani mwenu na mioyoni mwenu, mpate kuzitekeleza. “Leo hii nawapeni uchaguzi kati ya mema na mabaya; kati ya uhai na kifo. Kama mkitii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambazo ninawapa leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kufuata njia zake na kushika masharti na maagizo yake, basi, mtaishi na kuongezeka; naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawabariki katika nchi ambayo mnakwenda kuimiliki. Lakini mkipotoshwa na kukataa kumsikiliza, mkavutwa kuabudu miungu mingine na kuitumikia, mimi nawatangazieni leo hii kwamba mtaangamia. Hamtaishi kwa muda mrefu katika nchi mnayokwenda kuimiliki, ngambo ya mto wa Yordani. Naziita mbingu na dunia zishuhudie juu yenu leo hii, kwamba nimewapeni uchaguzi kati ya uhai na kifo, kati ya baraka na laana. Basi, chagueni uhai nyinyi na wazawa wenu mpate kuishi, mkimpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkiitii sauti yake na kuambatana naye. Maana kufanya hivyo kunamaanisha kwamba mtapata maisha marefu na kuishi katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliwaahidi wazee wenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo, kwamba atawapeni.” Mose aliendelea kuongea na Waisraeli wote, akawaambia, “Mimi sasa nina umri wa miaka 120, na sina nguvu ya kufanya kazi zaidi. Tena Mwenyezi-Mungu, ameniambia kuwa sitavuka mto Yordani. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawatangulia na kuyaangamiza mataifa yanayoishi huko, ili muimiliki nchi yao. Yoshua atakuwa kiongozi wenu kama alivyosema Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu atayaangamiza mataifa hayo kama vile alivyowaangamiza Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, na nchi yao. Mwenyezi-Mungu atawapeni ushindi juu yao nanyi mtawatendea kama nilivyowaamuru. Muwe imara na hodari, wala msiwaogope au kutishwa nao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ndiye anayekwenda pamoja nanyi. Yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa.” Kisha Mose akamwita Yoshua, akamwambia mbele ya watu wote wa Israeli, “Uwe Imara na hodari, maana wewe utawaongoza watu hawa kwenda kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliwaahidi babu zao; nawe utawakabidhi waimiliki. Mwenyezi-Mungu ndiye anayewaongoza; yeye atakuwa pamoja nanyi; yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa. Hivyo, msiogope wala msifadhaike.” Basi, Mose aliandika sheria hiyo, akawapa makuhani wa ukoo wa Lawi ambao walikuwa na jukumu la kubeba agano la Mwenyezi-Mungu, na wazee wote wa Israeli. Kisha akawaamuru akasema, “Kila mwaka wa saba utakuwa mwaka wa mafungulio. Katika sikukuu ya vibanda, mwaka huo, wakati watu wa Israeli wanapokuja mbele ya Mwenyezi-Mungu mahali pale atakapochagua mtawasomea watu wote wa Israeli sheria hii. Wakusanye watu: Wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili kila mmoja asikie maneno haya ya kujifunza kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuwa waangalifu kutekeleza maneno ya sheria hii. Nao wazawa wao ambao hawajasikia sheria ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, wapate kuisikia na kujifunza kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, muda wote mtakaoishi katika nchi ambayo mnakwenda kuimiliki ngambo ya mto Yordani.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Siku yako ya kuaga dunia imekaribia. Mwite Yoshua, mje pamoja katika hema la mkutano ili nimpe maagizo.” Basi, Mose na Yoshua wakaenda katika hema la mkutano, naye Mwenyezi-Mungu akawatokea humo katika nguzo ya wingu ambayo ilisimama kwenye mlango wa hema. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Umekaribia sasa kuaga dunia, na baada ya kufariki, watu wataanza kuniacha na kuiendea miungu mingine ya nchi hiyo ambamo watakwenda kuishi; wataniacha na kuvunja agano nililoagana nao. Hapo hasira yangu itawawakia siku hiyo, nami nitawaacha na kuuficha uso wangu mbali nao, wataangamizwa. Maovu mengi na taabu zitawavamia hata watambue kwamba maovu hayo yamewapata kwa kuwa Mungu wao hayupo miongoni mwao. Hakika nitawaficha uso wangu kwa sababu wamefanya mambo maovu na kuigeukia miungu mingine. “Sasa, andika wimbo huu, uwafundishe watu wa Israeli ili uwe ushahidi wangu juu yao. Nitakapowapeleka katika nchi inayotiririka maziwa na asali, kama nilivyowaapia babu zao, nao wakala wakashiba na kunenepa, wataigeukia miungu mingine na kuitumikia; watanidharau na kulivunja agano langu. Watakapovamiwa na maafa mengi na taabu, wimbo huu utawakabili kama ushahidi kwani hautasahauliwa na wazawa wao. Na hata sasa, kabla sijawapeleka katika nchi niliyoapa kuwapa, naijua mipango ambayo wanapanga.” Basi, Mose aliandika wimbo huo siku hiyohiyo, akawafundisha Waisraeli. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwagiza Yoshua, mwana wa Nuni, akamwambia, “Uwe imara na hodari, maana utawaongoza Waisraeli katika nchi ambayo nimewaapia kuwapa, nami nitakuwa pamoja nawe.” Mose alipomaliza kuandika maneno ya sheria hiyo tangu mwanzo mpaka mwisho, aliwaambia Walawi, waliokuwa na jukumu la kubeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, “Chukueni kitabu hiki cha sheria, mkiweke karibu na sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili kiwe ushahidi dhidi yenu. Maana najua mlivyo waasi na wakaidi. Ikiwa mmemwasi Mwenyezi-Mungu wakati niko hai pamoja nanyi, itakuwaje baada ya kifo changu? Wakusanye mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maofisa wenu nipate kusema maneno haya wasikie, nazo mbingu na dunia zishuhudie juu yao. Maana ninajua kuwa baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu na kuiacha ile njia niliyowaamuru mwifuate. Na katika siku zijazo mtakumbwa na maafa kwa kuwa mtafanya maovu mbele ya Bwana na kumkasirisha kwa matendo yenu.” Halafu, Mose akakariri maneno ya wimbo huu mbele ya kusanyiko lote la Waisraeli. “Tegeni masikio enyi mbingu: Sikiliza, ee dunia, maneno ninayosema. Mafundisho yangu na yatone kama mvua, maneno yangu yadondoke kama umande, kama manyunyu kwenye mimea michanga, kama mvua nyepesi katika majani mabichi. Maana nitalitangaza jina la Mwenyezi-Mungu, nanyi mseme, ‘Mungu wetu ni Mkuu’. “Mwenyezi-Mungu ni Mwamba wa usalama; kazi zake ni kamilifu, njia zake zote ni za haki. Yeye ni Mungu mwaminifu asiye na kosa, yeye hufanya mambo ya uadilifu na ya haki. Lakini nyinyi mmekosa uaminifu kwake, nyinyi sio watoto wake tena kwa sababu ya uovu, nyinyi ni kizazi kiovu na kipotovu. Mnawezaje kumlipa hivyo Mwenyezi-Mungu, enyi watu wapumbavu na msio na akili? Je, yeye siye Baba yenu aliyewaumba, aliyewafanya na kuwaimarisha? Kumbukeni siku zilizopita, fikirieni miaka ya vizazi vingi; waulizeni baba zenu nao watawajulisha, waulizeni wakubwa wenu nao watawaeleza. Mungu Mkuu alipoyagawia mataifa mali yao, alipowagawa wanadamu, kila taifa alilipatia mipaka yake, kulingana na idadi ya watoto wa Mungu, lakini alijiwekea watu wa Yakobo kuwa wake, hao alijichagulia kuwa mali yake. Aliwakuta katika nchi ya jangwa, nyika tupu zenye upepo mkali. Aliwalinda na kuwatunza, aliwafanya kama mboni ya jicho lake. Kama tai alindaye kiota chake, na kurukaruka juu ya makinda yake, akitandaza mabawa yake ili kuwashikilia, na kuwabeba juu ya mabawa yake. Yeye Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwaongoza na hapakuwa na mungu mwingine wa kumsaidia. Aliwapitisha katika nyanda za juu za nchi, nao wakala mazao ya mashambani. Akawapa asali miambani waonje na mafuta kutoka mwamba mgumu. Aliwapa siagi na maziwa ya mifugo, mafuta ya wanakondoo na kondoo madume, makundi ya mifugo ya Bashani na mbuzi. Aliwapa ngano nzuri kabisa na divai mpya wakanywa. Watu wa Israeli walinona na kupiga mateke; walinenepa, wakawa na kitambi na kunawiri; kisha wakamwacha Mungu aliyewaumba, wakamdharau Mwamba wa wokovu wao. Walimfanya aone wivu mkali kwa miungu yao, walimchochea akasirike kwa matendo yao ya kuchukiza. Walitambikia majini ambayo hayakuwa miungu, waliiendea miungu ambayo hawakuijua kamwe, miungu mipya iliyotokea siku za karibuni, ambayo wazee wao hawakuiheshimu kamwe. Hamkumjali Mwamba aliyewapa uhai, mlimsahau Mungu aliyewazaa nyinyi. Mwenyezi-Mungu aliona jambo hilo akawaacha; aliwakataa watoto wake, waume kwa wake. Akasema, ‘Nitawaficha uso wangu nione mwisho wao utakuwaje! Maana wao ni kizazi kipotovu, watoto wasio na uaminifu wowote. Wamenichochea kuona wivu kwa kitu kisicho mungu, wamenikasirisha kwa sanamu zao. Hivyo nitawafanya waone wivu kwa kisicho watu, nitawakasirisha kwa kutumia taifa la wapumbavu. Hasira yangu imewaka moto, inachoma mpaka chini kuzimu, itateketeza dunia na vilivyomo, itaunguza misingi ya milima. Nitarundika maafa chungu nzima juu yao, nitawamalizia mishale yangu. Watakonda kwa njaa, wataangamizwa kwa homa kali. Nitapeleka wanyama wenye meno makali kuwashambulia, na nyoka wenye sumu wanaotambaa mavumbini. Vita vitasababisha vifo vingi nje na majumbani hofu itawatawala, vijana wa kiume na wa kike watauawa hata wanyonyao na wazee wenye mvi. Nilisema, ningaliwaangamiza kabisa na kuwafanya wasikumbukwe tena na mtu yeyote, ila tu kwa sababu ya majivuno ya maadui zao ili maadui zao wasije wakafikiria vingine; wasije wakasema, wamefaulu kuwaangamiza, nami Mwenyezi-Mungu sihusiki katika mambo haya!’ “Israeli ni taifa lisilo na akili, watu wake hawana busara ndani yao. Wangekuwa na hekima wangejua kwa nini walishindwa, wangeweza kuelewa mwisho wao utakuwaje. Mtu mmoja anawezaje kuwashinda watu 1,000, au watu wawili wanawezaje kuwashinda watu 10,000, isipokuwa kama Mwamba wao amewatupa, Mwenyezi-Mungu wao amewaacha? Hata adui zetu wenyewe wamekiri wazi, mwamba wao hauna nguvu kama mwamba wetu. Maana mizabibu yao ni miche ya Sodoma zimetoka katika konde za Gomora; zabibu zake ni zabibu zenye sumu, vishada vyake ni vichungu. Divai yao ni kama sumu ya nyoka, ina sumu kali ya majoka. “Je sina njia ya kuwaadhibu? Silaha zangu ninazo mkononi. Kisasi ni juu yangu, mimi nitalipiza, wakati miguu yao itakapoteleza; maana siku yao ya maafa imewadia, mwisho wao u karibu sana. Mwenyezi-Mungu atawatetea watu wake, na kuwahurumia watumishi wake, wakati atakapoona nguvu zao zimeishia, wala hakuna aliyebaki, mfungwa au mtu huru. Ndipo Mwenyezi-Mungu atakapowauliza watu wake, ‘Iko wapi ile miungu yenu, mwamba mlioukimbilia usalama?’ Iko wapi hiyo miungu iliyokula matoleo yenu na kunywa divai na tambiko zenu za kinywaji? Basi na iinuke, iwasaidieni; acheni hiyo iwe kinga yenu sasa! Oneni kuwa mimi ndimi Mungu na wala hakuna mwingine ila mimi. Mimi huua na kuweka hai; hujeruhi na kuponya, na hakuna awezaye kumwokoa yeyote mikononi mwangu. Nanyosha mkono wangu mbinguni, na kuapa, kwa uhai wangu wa milele, kama mkiuona upanga wangu umeremetao, na kunyosha mkono kutoa hukumu, nitawalipiza kisasi maadui zangu, nitawaadhibu wale wanaonichukia. Mishale yangu nitailevya kwa damu, upanga wangu utashiba nyama, utalowa damu ya majeruhi na mateka na adui wenye nywele ndefu. “Enyi mataifa washangilieni watu wake, maana yeye hulipiza kisasi damu ya watumishi wake, huwalipiza kisasi wapinzani wake, na kuitakasa nchi ya watu wake.” Mose alikuja mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, wakakariri maneno ya wimbo huu, ili Waisraeli wote wausikie. Mose alipomaliza kuwaambia watu wa Israeli maneno haya yote, aliwaambia, “Yawekeni mioyoni mwenu maneno yote ambayo ninawapeni leo. Lazima muwaamuru watoto wenu ili wafuate kwa uaminifu maneno yote ya sheria hii. Maana sheria hii si maneno matupu bali ni uhai wenu; kwa sheria hii mtaishi maisha marefu katika nchi mnayokwenda kuimiliki, ngambo ya mto Yordani.” Siku hiyohiyo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Panda mlima huu wa Abarimu, mlima Nebo katika nchi ya Moabu, mkabala wa mji Yeriko, ukaiangalie nchi ya Kanaani ninayowapa Waisraeli waimiliki. Kisha ufariki hukohuko mlimani kama kaka yako Aroni alivyofariki katika mlima Hori, kwa sababu nyote wawili mlivunja uaminifu wenu kwangu mbele ya Waisraeli mlipokuwa kwenye maji ya Meriba, karibu na mji wa Kadeshi, katika jangwa la Sini, mkakosa kuuthibitisha utakatifu wangu kati ya Waisraeli. Utaiona nchi iliyo mbele yako, lakini hutaingia katika nchi hiyo ninayowapa Waisraeli.” Hii ndiyo baraka ambayo Mose, mtu wa Mungu aliwatakia Waisraeli kabla ya kufariki kwake. Alisema: Mwenyezi-Mungu alikuja kutoka mlima Sinai, alitutokea kutoka mlima Seiri; aliiangaza kutoka mlima Parani. Alitokea kati ya maelfu ya malaika, na moto uwakao katika mkono wake wa kulia. Mwenyezi-Mungu aliwapenda watu wake; na huwalinda watakatifu wake wote. Hivyo, malaika wake walifuata nyayo zake, na kupata maagizo kutoka kwake. Mose alituamuru tutii sheria; kitu cha thamani kuu cha taifa letu. Mwenyezi-Mungu akawa mfalme wa Israeli, wakati viongozi wao walipokutana, na makabila yote yalipokusanyika. Mose alisema juu ya kabila la Reubeni: “Reubeni aishi wala asife, na watu wake wasiwe wachache.” Juu ya kabila la Yuda alisema: “Ee Mwenyezi-Mungu usikilize kilio cha kabila la Yuda; umrudishe tena kwa watu wale wengine. Upigane kwa mikono yako kwa ajili yake, ulisaidie kabila la Yuda dhidi ya adui zake.” Juu ya kabila la Lawi, alisema: “Ee Mwenyezi-Mungu ulipatie Lawi kauli yako ya Urimu, kauli yako ya thumimu kwa hao waaminifu wako, ambao uliwajaribu huko Masa. Ulishindana nao kwenye maji ya Meriba. Walawi walioamua kuwaacha wazee wao, wakawasahau jamaa zao, wasiwatambue hata watoto wao maana walizingatia amri zako, na kushika agano lako. Na wawafundishe wazawa wa Yakobo maagizo yako; wawafundishe watu wa Israeli sheria yako. Walawi na wafukize ubani mbele yako, sadaka nzima za kuteketezwa madhabahuni pako. Ee Mwenyezi-Mungu, uzibariki nguvu zao, uzikubali kazi za mikono yao; uzivunjilie mbali nguvu za maadui zao, nguvu za wanaowachukia hata wasiinuke tena.” Juu ya kabila la Benyamini alisema: “Hili ni kabila alipendalo Mwenyezi-Mungu, nalo hukaa salama karibu naye. Yeye hulilinda mchana kutwa, na kukaa kati ya milima yake.” Juu ya kabila la Yosefu alisema: “Mwenyezi-Mungu na aibariki nchi yake, kwa baraka nzuri kabisa kutoka juu, ibarikiwe kwa matunda bora yalioiva kwa jua, kwa matunda ya kila mwezi; kwa mazao bora ya milima ya kale, na mazao tele ya milima ya kale, Nchi yake ijae yote yaliyo mema, ibarikiwe kwa wema wa Mwenyezi-Mungu, ambaye alitokea katika kichaka. Baraka hizi ziwashukie watu wa kabila la Yosefu, aliyekuwa mkuu miongoni mwa ndugu zake. Fahari yake ni fahari ya fahali wa kwanza, pembe zake ni za nyati dume. Atazitumia kuyasukuma mataifa; yote atayasukuma mpaka miisho ya dunia. Efraimu atakuwa na pembe hizo 10,000 na Manase kwa maelfu.” Juu ya kabila la Zebuluni na kabila la Isakari, alisema, “Zebuluni, furahi katika safari zako; nawe Isakari, furahi katika mahema yako. Watawaalika wageni kwenye milima yao, na huko watu watatoa sadaka zinazotakiwa. Maana wao watapata utajiri wao kutoka baharini na hazina zao katika mchanga wa pwani.” Juu ya kabila la Gadi, alisema: “Atukuzwe Mungu ampatiaye Gadi sehemu kubwa. Gadi hunyemelea kama simba akwanyue mkono na utosi wa kichwa. Alijichagulia eneo zuri kuliko yote, mahali ilipotengwa sehemu ya kiongozi. Aliwaongoza watu na kumtii Mwenyezi-Mungu, alitekeleza mpango wa Mungu kwa Israeli.” Juu ya kabila la Dani alisema hivi: “Dani ni mwanasimba arukaye kutoka Bashani.” Juu ya kabila la Naftali alisema: “Ee Naftali fadhili, uliyejaa baraka za Mwenyezi-Mungu, nchi yako ni kusini kwenye ziwa Kinerethi.” Juu ya kabila la Asheri alisema: “Asheri abarikiwe kuliko watoto wote wa Yakobo, na upendelewe na ndugu zako wote; na achovye mguu wake katika mafuta. Miji yako ni ngome za chuma na shaba. Usalama wako utadumu maisha yako yote!” Mose akamalizia kwa kusema, “Ee Israeli, hakuna aliye kama Mungu wako, yeye hupita mbinguni kuja kukusaidia, hupita juu angani katika utukufu wake. Mungu wa milele ndiye kimbilio lenu; nguvu yake yaonekana duniani. Aliwafukuza maadui mbele yenu; aliwaamuru: ‘Waangamizeni.’ Kwa hiyo, watu wa Israeli wakakaa salama, wazawa wa Yakobo peke yao, katika nchi iliyojaa nafaka na divai, nchi ambayo anga lake hudondosha umande. Heri yenu nyinyi Waisraeli. Nani aliye kama nyinyi, watu mliookolewa na Mwenyezi-Mungu, ambaye ndiye ngao ya msaada wenu, na upanga unaowaletea ushindi! Adui zenu watakuja wananyenyekea mbele yenu, nanyi mtawakanyaga chini.” Basi, Mose akaondoka kwenye tambarare ya Moabu, akaenda mlimani Nebo, akapanda kilele cha Pisga kilicho mkabala wa Yeriko. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwonesha nchi yote: Toka Gileadi mpaka Dani; eneo lote la Naftali, eneo la Efraimu na Manase, eneo lote la Yuda mpaka Bahari ya Mediteranea; nyika ya Negebu na eneo la nyika ya bonde la Yeriko, mji wa mitende, mpaka Soari. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Hii ndiyo nchi ile niliyomwapia Abrahamu, Isaka na Yakobo kwamba nitawapa wazawa wao. Nimekuonesha uione kwa macho yako mwenyewe, lakini hutafika huko.” Basi, Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu akafariki huko nchini Moabu, kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amemesema. Mwenyezi-Mungu akamzika katika bonde la Moabu, mkabala na mji wa Beth-peori; lakini mpaka leo, hakuna mtu ajuaye mahali alipozikwa. Mose alikuwa na umri wa miaka 120 alipofariki; macho yake yalikuwa hayajafifia, na alikuwa timamu na mwenye nguvu. Waisraeli waliomboleza kifo chake kwa muda wa siku thelathini kwenye nchi tambarare ya Moabu. Kisha siku za matanga na maombolezo ya kifo chake zikaisha. Yoshua mwana wa Nuni alijaa roho ya hekima, kwa kuwa Mose alikuwa amemwekea mikono yake. Hivyo Waisraeli walimtii Yoshua na kufuata amri ambazo Mwenyezi-Mungu alimpa Mose. Hapajatokea tena nabii katika Israeli kama Mose, ambaye Mwenyezi-Mungu aliongea naye ana kwa ana. Hakuna nabii mwingine ambaye alifanya ishara na miujiza kama ile ambayo Mwenyezi-Mungu aliyomtuma Mose afanye juu ya mfalme wa Misri, wakuu wake na nchi yake yote. Hakuna nabii mwingine ambaye amefanya mambo makuu na ya kutisha kama alivyofanya Mose mbele ya Waisraeli wote. Baada ya kifo cha Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu alimwambia Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Mose: “Mtumishi wangu Mose amefariki, sasa vukeni mto Yordani, wewe pamoja na Waisraeli wote hadi kwenye nchi ile ambayo ninawapa. Kila mahali mtakapokanyaga nimewapeni kama nilivyomwahidi Mose. Mipaka ya nchi yenu itakuwa hivi: Kusini ni jangwa, kaskazini ni milima ya Lebanoni, mashariki ni mto ule mkubwa Eufrate, kupitia nchi yote ya Wahiti hadi bahari ya Mediteranea upande wa magharibi. Hakuna mtu atakayekushinda siku zote za maisha yako. Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose. Daima nitakuwa nawe wala sitakuacha kamwe. Uwe imara na hodari kwa kuwa wewe utawaongoza watu hawa kuirithi nchi ambayo niliwaahidi wazee wao kuwa nitawapa. Ila tu, uwe imara na hodari; uwe mwangalifu na kuzingatia sheria yote aliyokuamuru mtumishi wangu Mose. Fuata kila sehemu ya sheria hiyo nawe utafanikiwa popote uendapo. Hakikisha kuwa hutakisahau kamwe kitabu hiki cha sheria; bali kila siku utajifunza kitabu hiki, mchana na usiku, ili upate kutekeleza yote yaliyoandikwa humu, nawe utafanikiwa na kustawi popote uendapo. Kumbuka kuwa mimi nimekuamuru uwe imara na hodari. Usiogope wala usifadhaike kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niko pamoja nawe popote uendapo.” Kisha Yoshua akawaamuru viongozi wa watu, “Piteni katika kambi na kuwaamrisha watu watayarishe chakula, kwa kuwa baada ya siku tatu mtavuka mto Yordani, kwenda kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapeni iwe mali yenu.” Yoshua akawaambia watu wa kabila la Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase: “Kumbukeni lile jambo ambalo Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliwaamuru akisema, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa mahali pa kupumzika, na atawapa nchi hii’. Wake zenu, watoto wenu na wanyama wenu wa kufugwa watabaki katika nchi hiyo ambayo Mose aliwapeni, ngambo ya mto Yordani. Lakini wanaume wote hodari wakiwa na silaha watavuka mto na kuwatangulia ndugu zenu. Mtawasaidia mpaka Mwenyezi-Mungu atakapowapa ndugu zenu pia mahali pa kupumzikia, kama alivyowapa nyinyi, nao pia wamiliki nchi ambayo wanapewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kisha mtarudi katika nchi ambayo ni mali yenu na kuimiliki, nchi ambayo mlipewa na Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, mashariki ya mto Yordani.” Wakamjibu Yoshua, “Mambo yote uliyotuamuru tutayafanya, na popote utakapotutuma tutakwenda. Kama vile tulivyomtii Mose katika mambo yote, ndivyo tutakavyokutii wewe; Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na Mose. Mtu yeyote atakayeasi amri yako au kukataa kutii maneno yako au jambo lolote unalomwamuru, atauawa. Wewe, lakini, uwe na nguvu na kuwa hodari.” Basi, Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kwa siri kutoka Shitimu waende kufanya upelelezi, katika nchi ile na hasa mji wa Yeriko. Wakaenda, wakafika kwenye nyumba ya malaya mmoja aliyeitwa Rahabu wakalala humo. Mfalme wa mji wa Yeriko akaambiwa, “Tazama, wanaume wawili Waisraeli wameingia mjini leo usiku ili kuipeleleza nchi.” Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akisema: “Watoe nje watu waliokuja nyumbani kwako kwani wamekuja kuipeleleza nchi yote.” Lakini, yule mwanamke alikuwa amekwisha waficha watu hao wawili. Basi, akawaambia wajumbe hao, “Ni kweli kwamba hao watu walikuja kwangu, lakini mimi sikujua wametoka wapi. Wakati wa kufunga lango la mji, giza lilipoingia, hao watu waliondoka. Kule walikokwenda mimi sijui; wafuateni upesi nanyi mtawapata.” Lakini Rahabu alikuwa amewapandisha hao wapelelezi kwenye paa na kuwaficha kwa mabua ya kitani aliyokuwa ameyatandaza huko paani. Basi, wale watu waliotumwa na mfalme wakawafuatia kwa kupitia njia iliyokuwa imeelekea kwenye vivuko vya Yordani. Na mara tu walipoondoka mjini, lango la mji likafungwa. Rahabu akawaendea hao wapelelezi juu darini kabla hawajalala, akawaambia, “Mimi ninajua kwamba Mwenyezi-Mungu amewapa nchi hii; tumekumbwa na hofu juu yenu na wakazi wote wa nchi hii wamekufa moyo kwa sababu yenu. Maana tumesikia jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu mlipotoka nchi ya Misri, na jinsi mlivyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, yaani Sihoni na Ogu, ambao mliwaangamiza kabisa. Mara tu tuliposikia mambo hayo, tulikufa moyo kabisa kwa sababu yenu, tukaishiwa nguvu kabisa. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu juu mbinguni na chini duniani! Kwa hiyo basi, tafadhali mniapie kwa jina la Mwenyezi-Mungu kwamba mtanitendea kwa wema mimi na jamaa yangu kama vile mimi nilivyowatendeeni kwa wema, na mnipe uthibitisho kamili. Ahidini kwamba mtamsalimisha baba yangu na mama yangu, kaka zangu na dada zangu, na jamaa yao yote; hamtakubali tuuawe!” Wale watu wakamjibu, “Uhai wenu ni uhai wetu! Kama hamtaifichua siri yetu, Mwenyezi-Mungu atakapotupa nchi hii, tutakutendea kwa wema na uaminifu.” Basi, Rahabu akawashusha hao watu kwa kamba kupitia dirishani, kwa kuwa nyumba yake ilikuwa imejengwa ikiambatana na ukuta wa mji wa Yeriko. Akawaambia: “Nendeni mlimani mkajifiche huko ili wanaowafuatia wasiwakute. Kaeni huko kwa muda wa siku tatu, mpaka wanaowafuatia watakapokuwa wamerudi mjini, kisha mwende zenu.” Hao watu wakamwambia, “Sisi tutalitimiza kabisa jambo ulilotufanya tuahidi kwa kiapo. Tutakapokuja katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu kwenye dirisha ambalo umetuteremshia. Uwakusanye hapa kwako baba yako, mama yako na kaka zako na jamaa yote ya baba yako. Lakini mtu yeyote akitoka nje ya nyumba yako na kwenda mitaani hatutakuwa na lawama juu ya kifo chake. Lakini kama mtu yeyote atakayekuwamo ndani ya nyumba yako akiguswa tu, basi lawama ya kifo chake itakuwa juu yetu. Lakini kama ukimwambia mtu yeyote juu ya shughuli hii yetu, basi, sisi hatutabanwa na kiapo ulichotufanya tukuapie.” Naye akawaambia “Na iwe jinsi mlivyosema.” Kisha akawaruhusu waende zao, nao wakaondoka. Naye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani. Wapelelezi hao waliondoka wakaenda milimani. Walikaa huko kwa muda wa siku tatu mpaka wale waliokuwa wanawafuatia waliporudi mjini Yeriko, baada ya kuwatafuta na kukosa kuwaona. Basi, hao wapelelezi wawili wakashuka kutoka milimani, wakavuka mto na kumwendea Yoshua, mwana wa Nuni; wakamwambia yote yaliyowapata. Wakamwambia “Hakika Mwenyezi-Mungu ameitia nchi yote mikononi mwetu. Tena wakazi wa nchi hiyo wamekufa moyo kwa sababu yetu.” Asubuhi na mapema Yoshua pamoja na watu wote wa Israeli walianza safari kutoka Shitimu. Walipoufikia mto Yordani, walipiga kambi hapo kwa muda kabla ya kuvuka. Baada ya siku tatu, viongozi walipita katikati ya kambi hiyo, wakawaambia watu, “Mtakapoliona sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, limebebwa na makuhani Walawi, mtaondoka na kulifuata; ndivyo mtakavyojua njia ya kupita maana hamjapita huku kamwe. Lakini msilikaribie mno sanduku la agano; muwe umbali wa kilomita moja hivi.” Yoshua akawaambia watu, “Jitakaseni kwa kuwa kesho Mwenyezi-Mungu atatenda maajabu kati yenu.” Kisha akawaambia makuhani, “Chukueni sanduku la agano, mtangulie nalo mbele ya watu.” Nao wakalichukua na kutangulia mbele ya watu. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua: “Leo hii, nitaanza kukutukuza mbele ya watu wote wa Israeli ili wajue kwamba, kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo pia nitakavyokuwa pamoja nawe. Utawaamuru hao makuhani wanaobeba sanduku la agano wasimame karibu na ukingo wa mto Yordani wakati watakapofika huko.” Kisha Yoshua akawaambia Waisraeli: “Njoni karibu mpate kusikia maneno ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Yoshua akaendelea kusema, “Sasa mtajulishwa kabisa kwamba Mungu aliye hai yu miongoni mwenu na kwamba atawafukuza mbele yenu Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi, bila kushindwa. Tazameni, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote, liko karibu kupita mbele yenu kuelekea mtoni Yordani. Sasa, chagueni watu kumi na wawili kutoka makabila ya Israeli, kila kabila mtu mmoja. Wakati nyayo za makuhani wanaobeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Bwana wa dunia yote, zitakapoingia katika maji ya mto Yordani, maji ya mto huo yataacha kutiririka. Na yale yatakayokuwa yanatiririka kutoka upande wa juu yatajikusanya pamoja kama rundo.” Basi, watu waliondoka katika kambi zao ili kwenda kuvuka mto Yordani, nao makuhani wakiwa wamebeba sanduku la agano wanawatangulia watu. Na mara tu hao waliobeba sanduku la agano walipofika Yordani na nyayo zao zilipokanyaga ukingoni mwa mto huo (mto Yordani hufurika wakati wa mavuno), maji yaliyokuwa yanatiririka kutoka upande wa juu yalisimama na kurundikana mpaka huko Adamu kijiji kilicho karibu na mji wa Sarethani. Maji yaliyokuwa yanateremka kwenda bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yalitoweka kabisa, watu wakavuka mbele ya Yeriko. Wakati Waisraeli walipokuwa wanavuka makuhani waliokuwa wanalibeba sanduku la agano walisimama mahali pakavu katikati ya mto Yordani mpaka taifa lote likavuka. Taifa zima lilipokwisha vuka mto Yordani, Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa hao Waisraeli, yaani mtu mmoja kutoka kila kabila, uwaagize hivi, ‘Chukueni mawe kumi na mawili kutoka hapa katikati ya mto Yordani, kutoka hapa ilipo miguu ya makuhani, muyachukue mawe hayo, mkayaweke mahali pale ambapo mtalala leo hii.’” Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili ambao alikuwa amewateua miongoni mwa Waisraeli, kila kabila mtu mmoja, akawaambia, “Litangulieni sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mpaka katikati ya mto Yordani. Kila mmoja wenu achukue jiwe begani mwake, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli. Jambo hilo litakuwa ishara kati yenu; na watoto wenu watakapowauliza siku zijazo ‘Je, mawe haya yana maana gani kwenu?’ Nyinyi mtawaambia, ‘Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipopitishwa mtoni Yordani, maji ya mto huo yalizuiliwa yasitiririke!’ Kwa hiyo mawe haya yatakuwa ukumbusho kwa Waisraeli milele.” Wale wanaume wakafanya kama walivyoamriwa na Yoshua, wakachukua mawe kumi na mawili kutoka katikati ya mto Yordani, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Yoshua, wakaenda nayo hadi mahali pale walipolala, wakayaweka huko. Yoshua akasimika pia mawe kumi na mawili katikati ya mto Yordani, mahali pale ambapo nyayo za makuhani waliobeba lile sanduku la agano zilisimama. Mawe hayo yako huko mpaka hivi leo. Wale makuhani waliobeba sanduku la agano, walisimama katikati ya mto Yordani mpaka watu walipomaliza kutekeleza kila kitu ambacho Mwenyezi-Mungu alimwamuru Yoshua awaambie watu; Yoshua alifanya yote ambayo Mose alikuwa amemwamuru. Watu wakaharakisha kuvuka mto, na watu wote walipokwisha vuka, wale makuhani wakawatangulia na lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Wanaume wa kabila la Reubeni na la Gadi na nusu ya kabila la Manase waliwatangulia Waisraeli wakiwa na silaha zao, kama vile walivyoagizwa na Mose. Watu wapatao 40,000 wakiwa na silaha tayari kwa vita walipita mbele ya Mwenyezi-Mungu wakielekea bonde la mji wa Yeriko. Katika siku hiyo Mwenyezi-Mungu akamtukuza Yoshua mbele ya Waisraeli wote, nao wakamheshimu Yoshua maisha yake yote kama walivyomheshimu Mose maishani mwake. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Yoshua, “Waamuru makuhani wanaobeba sanduku la maamuzi, watoke mtoni Yordani.” Basi, Yoshua akawaamuru wale makuhani, “Tokeni mtoni Yordani.” Hao makuhani waliokuwa wamebeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu walipotoka katikati ya mto Yordani, na kukanyaga ukingo wa mto, maji ya mto Yordani yakaanza kutiririka tena, na kufurika kama kwanza. Waisraeli walivuka mto Yordani katika siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga kambi huko mjini Gilgali, mashariki ya Yeriko. Yoshua akayasimika yale mawe kumi na mawili ambayo waliyachukua kutoka mtoni Yordani, huko Gilgali. Kisha Yoshua akawaambia Waisraeli, “Watoto wenu watakapowaulizeni siku zijazo, ‘Je, mawe haya yana maana gani?’ Mtawaambia hivi: ‘Taifa la Israeli lilivuka mto huu wa Yordani mahali pakavu.’ Mtawaambia kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyakausha maji ya mto Yordani kwa ajili yenu mpaka mkavuka, kama alivyokausha bahari ya Shamu, kwa ajili yetu tukavuka, ili watu wote wa dunia wajue kuwa mkono wa Mwenyezi-Mungu una nguvu; nanyi mpate kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, milele.” Wafalme wote wa Waamori walioishi ngambo ya magharibi ya Yordani, na wafalme wote wa Wakanaani waliokuwa pwani ya bahari ya Mediteranea, waliposikia kwamba Mwenyezi-Mungu aliyakausha maji ya mto Yordani kwa ajili ya Waisraeli mpaka walipokwisha vuka, wakafa moyo; wakaishiwa nguvu kabisa kwa kuwaogopa Waisraeli. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya jiwe gumu ili uwatahiri Waisraeli.” Basi, Yoshua akatengeneza visu hivyo vya jiwe gumu na kuwatahiri Waisraeli huko Gibea-haaralothi. Sababu ya kuwatahiri Waisraeli ni hii: Waisraeli wote, wanaume, waliotoka Misri ambao walikuwa na umri wa kwenda vitani, wote walifariki safarini jangwani baada ya kutoka nchini Misri. Hao wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini wale wote waliozaliwa safarini huko jangwani baada ya kutoka Misri, walikuwa bado hawajatahiriwa. Waisraeli walisafiri kwa muda wa miaka arubaini nyikani hata wanaume wote waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakaangamia kwa kuwa hawakusikiliza aliyosema Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu alikuwa amewaapia watu hao kwamba hawataiona nchi ile inayotiririka maziwa na asali ambayo yeye aliwaapia baba zao kuwa atawapa. Kwa hiyo ilikuwa ni watoto wa watu hao ambao Mwenyezi-Mungu aliwakuza badala yao, hao ndio Yoshua aliwatahiri, kwani hawakuwa wametahiriwa wakati ule walipokuwa safarini jangwani. Wanaume wote walipokwisha tahiriwa walikaa katika sehemu zao humo kambini mpaka walipopona. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Leo hii nimewaondoleeni ile aibu ya Misri.” Hivyo mahali hapo pakaitwa Gilgali mpaka hivi leo. Waisraeli walipokuwa wamepiga kambi huko Gilgali waliadhimisha sikukuu ya Pasaka jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi katika tambarare za Yeriko. Kesho yake, yaani baada ya Pasaka, walikula mikate isiyotiwa chachu na bisi kutokana na mazao ya nchi ile. Basi, tangu siku hiyo walipokula mazao ya nchi hiyo Waisraeli hawakupata mana tena. Tangu mwaka huo Waisraeli walikula mazao ya nchi ya Kanaani. Siku moja Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, ghafla aliona mtu mmoja amesimama mbele yake na upanga uliofutwa mkononi mwake. Yoshua akamwendea, akamwuliza, “Je, wewe ni wetu au ni wa adui zetu?” Naye akamjibu; “Wala wenu wala wa adui zenu! Ila mimi ni kamanda wa jeshi la Mwenyezi-Mungu, na sasa nimewasili.” Yoshua akainama chini akasujudu, kisha akamwuliza, “Bwana wangu, mimi mtumishi wako, unataka nifanye nini?” Huyo kamanda wa jeshi la Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Vua viatu vyako kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.” Yoshua akafanya hivyo. Milango ya kuingilia mjini Yeriko ilikuwa imefungwa imara kwa ndani kuwazuia Waisraeli wasiingie. Hakuna mtu aliyeweza kuingia wala kutoka katika mji huo. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Angalia! Mimi nitautia mikononi mwako mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake na askari wake shujaa. Wewe na wale watu wenye silaha wote mtauzunguka huo mji mara moja kila siku kwa siku sita. Makuhani saba, kila mmoja akiwa amechukua baragumu yake ya pembe za kondoo dume, watatangulia mbele ya sanduku la agano. Katika siku ya saba mtauzunguka mji huo mara saba, huku makuhani wakipiga mabaragumu. Watakapopiga hayo mabaragumu kwa mlio mkubwa na mara tu mtakaposikia huo mlio, watu wote watapiga kelele kubwa, nazo kuta za mji zitaanguka chini. Ndipo watu watauvamia mji kila mmoja kutoka mahali aliposimama.” Basi, Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, “Libebeni sanduku la agano na makuhani saba wachukue mabaragumu saba za kondoo dume, watangulie mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu.” Yoshua akawaambia watu, “Nendeni mbele; uzungukeni mji, nao watu wenye silaha waende mbele ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.” Kulingana na amri ya Yoshua, wale makuhani saba waliokuwa na mabaragumu saba ya kondoo dume wakaenda mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakiwa wanapiga mabaragumu, nyuma yao wakifuatwa na lile sanduku la agano. Wale watu wenye silaha wakawatangulia wale makuhani ambao walikuwa wanapiga mabaragumu, na walinzi wengine wakifuata nyuma ya sanduku hilo, huku mabaragumu yakilia kwa mfululizo. Lakini Yoshua akawaamuru watu, “Msipige kelele au kutoa sauti, wala neno lolote lisitoke vinywani mwenu, mpaka siku ile ambapo nitawaambieni mpige kelele; wakati huo ndipo mtakapopiga kelele.” Basi, Yoshua aliwafanya wale watu wauzunguke mji mara moja kila siku wakiwa wamebeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu na kurudi kambini kulala usiku. Asubuhi yake Yoshua akaamka alfajiri na mapema, na makuhani wakalibeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Wale makuhani saba wenye mabaragumu saba za kondoo dume walitembea mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu wakipiga mabaragumu mfululizo. Watu wenye silaha walilitangulia sanduku la Mwenyezi-Mungu na walinzi wengine nyuma yake. Mabaragumu yakaendelea kupigwa. Siku ya pili yake waliuzunguka huo mji mara moja; na kurudi tena kambini kwao. Walifanya hivyo kwa muda wa siku sita. Siku ya saba, waliamka alfajiri na mapema, wakauzunguka mji huo mara saba kwa namna ileile. Ilikuwa ni siku hiyo tu ambayo waliuzunguka mji huo mara saba. Ilipofika mara ya saba, wakati makuhani walipokwisha piga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, “Pigeni kelele, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha wapeni huu mji! Mji huo utaangamizwa na kila kitu kilichomo kwani umewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Rahabu, yule kahaba, ndiye atakayesalimishwa pamoja na wale ambao wamo nyumbani mwake kwa kuwa aliwaficha wapelelezi wetu. Lakini msichukue chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe, mkichukua kitu chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe mtaifanya kambi ya Israeli kuwa kitu cha kuangamizwa, na hivyo kuiletea balaa. Lakini fedha yote, dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu; hivyo vitawekwa katika hazina ya Mwenyezi-Mungu.” Basi, watu wakapiga kelele huku mabaragumu yanapigwa. Watu waliposikia sauti ya mabaragumu walipiga kelele kubwa, na kuta za mji zikaanguka chini kabisa. Mara watu wakauvamia mji, kila mmoja kutoka mahali aliposimama, wakauteka. Kisha wakaangamiza kila kitu mjini humo na kuwaua kwa upanga: Wanaume na wanawake, vijana na wazee, ng'ombe, kondoo na punda. Yoshua akawaambia wale wapelelezi wawili walioipeleleza nchi hiyo, “Nendeni katika nyumba ya yule kahaba; mkamlete yule mwanamke na wale wote ambao ni ndugu zake kama mlivyomwapia.” Basi, wale vijana wapelelezi wakaenda; wakamleta Rahabu, baba yake na mama yake, ndugu zake na watu wote wa jamaa yake, wakawaweka nje ya kambi ya Israeli. Kisha, wakauchoma moto mji wa Yeriko na kila kitu kilichokuwako isipokuwa fedha, dhahabu, vyombo vya shaba na vya chuma; hivyo viliwekwa katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Lakini yule kahaba Rahabu pamoja na watu wote wa nyumba ya baba yake, Yoshua aliyaokoa maisha yao. Rahabu akaishi miongoni mwa Waisraeli hadi leo, kwa kuwa aliwaficha wajumbe ambao Yoshua aliwatuma kwenda kuupeleleza mji wa Yeriko. Wakati huo Yoshua alitamka apizo rasmi mbele ya watu akisema, “Atakayeujenga tena mji wa Yeriko, na alaaniwe na Mungu, Yeyote atakayeweka msingi wa mji huo, mzaliwa wake wa kwanza na afe. Yeyote atakayejenga lango la mji huo, mwanawe kitinda mimba na afe.” Basi, Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yoshua na sifa zake zikaenea nchini kote. Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyotolewa viangamizwe kwani Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alichukua baadhi ya vitu vilivyoamriwa viteketezwe. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Waisraeli. Yoshua akawatuma watu kutoka Yeriko kwenda mji wa Ai, ulio karibu ya Beth-aveni, mashariki ya Betheli, akawaambia, “Nendeni mkaipeleleze nchi.” Nao wakaenda na kuupeleleza mji wa Ai. Waliporudi, wakamwambia Yoshua, “Hakuna haja kupeleka watu wote kuushambulia mji wa Ai, maana wakazi wake ni wachache tu. Watu elfu mbili au tatu watatosha.” Basi, watu kama elfu tatu hivi wakaenda kuushambulia mji wa Ai, lakini wakakimbizwa na wakazi wa mji huo. Watu wa Ai wakawaua Waisraeli thelathini na sita na kuwafukuza wengine kutoka lango la mji mpaka Shebarimu, wakawaua kwenye mteremko. Waisraeli wakafa moyo na kulegea kama maji. Yoshua akayararua mavazi yake, yeye pamoja na wazee wa Israeli. Wakajitupa chini mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu mpaka jioni; wakajitia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, “Ole wetu, ee Bwana Mungu! Kwa nini umetuvusha mto Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Tungaliridhika kubaki ngambo ya mto Yordani! Ee Bwana, niseme nini hali Waisraeli wamewakimbia adui zao? Basi, Wakanaani pamoja na wakazi wote wa nchi hii watakapopata habari hiyo watatuzingira na kutufuta kabisa duniani. Sasa utafanya nini kuonesha ukuu wa jina lako?” Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Simama! Mbona umejitupa chini hivyo? Waisraeli wametenda dhambi, maana wamelivunja agano langu nililowaamuru washike; wamevichukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu viangamizwe; wameviiba na kudanganya, wakaviweka pamoja na vitu vyao. Kwa hiyo Waisraeli hawawezi kuwakabili maadui zao; wanawakimbia adui zao kwa sababu wamejifanya wenyewe kuwa kitu cha kuangamizwa! Sitakuwa pamoja nao tena msipoharibu vitu vilivyomo kati yenu vilivyotolewa viangamizwe. Basi, inuka uwatakase watu, waambie wajitakase na kujitayarisha kwa siku ya kesho, maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: ‘Miongoni mwenu kuna vitu vilivyotolewa viangamizwe; hamwezi kuwakabili adui zenu mpaka vitu hivyo vimeondolewa kati yenu! Kwa hiyo kesho asubuhi wote mtakuja mbele yangu, kabila baada ya kabila. Kabila nitakalolichagua litakwenda mbele, ukoo baada ya ukoo. Ukoo nitakaouchagua utakwenda mbele, jamaa baada ya jamaa. Na jamaa nitakayoichagua itakwenda mbele, mtu mmojammoja. Mtu yeyote atakayepatikana akiwa na vitu vilivyotolewa viangamizwe atateketezwa kwa moto, yeye pamoja na kila kitu chake maana ameliasi agano langu mimi Mwenyezi-Mungu, akatenda jambo la aibu katika Israeli.’” Basi, Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawaleta Waisraeli wote karibu, kabila baada ya kabila; kabila la Yuda likachaguliwa. Akazileta karibu koo za Yuda, ukoo baada ya ukoo; na ukoo wa Zerahi ukachaguliwa. Akazileta karibu jamaa za ukoo wa Zerahi, jamaa baada ya jamaa; na jamaa ya Zabdi ikachaguliwa. Yoshua akaileta jamaa ya Zabdi karibu, nyumba baada ya nyumba; na nyumba ya Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, ikachaguliwa. Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, msifu na kisha uniambie yale uliyotenda, wala usinifiche.” Akani akamjibu; “Ni kweli nimetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Na hivi ndivyo nilivyofanya: Nilipoona vazi moja zuri kutoka Shinari kati ya nyara, shekeli 200 za fedha na mchi wa dhahabu wenye uzito wa shekeli 50, nikavitamani na kuvichukua; nimevificha ardhini ndani ya hema langu; na fedha iko chini ya vitu hivyo.” Basi, Yoshua akawatuma wajumbe, nao wakakimbia hemani kwa Akani. Na kumbe, vilikuwa vimefichwa hemani na fedha ikiwa chini yake. Wakavichukua hemani na kuvipeleka kwa Yoshua na watu wote wa Israeli; nao wakaviweka chini, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Yoshua pamoja na Waisraeli wote, wakamchukua Akani, mwana wa Zera, pamoja na fedha, vazi, dhahabu, watoto wake wa kiume na binti zake, ng'ombe, punda na kondoo wake, hema lake na kila kitu alichokuwa nacho na kuwapeleka kwenye bonde la Akori. Yoshua akamwuliza Akani, “Kwa nini umetuletea taabu? Mwenyezi-Mungu atakuletea taabu wewe mwenyewe leo.” Waisraeli wote wakampiga Akani kwa mawe mpaka akafa. Kisha wakawapiga jamaa yake yote kwa mawe mpaka wakafa, wakawateketeza wote kwa moto. Halafu wakarundika mawe mengi juu yake, ambayo yako hadi leo. Hapo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikapoa; na mahali hapo pakaitwa Bonde la Akori mpaka hivi leo. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usiwe na wasiwasi wowote; wachukue wanajeshi wako wote uelekee mji wa Ai, kwani mfalme wa Ai nimemtia mikononi mwako, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake. Mtautendea mji wa Ai pamoja na mfalme wake kama vile mlivyoutendea mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake. Mali zake pamoja na mifugo yake mtakayoteka itakuwa ni mali yenu. Nendeni mwuvamie mji kutoka upande wa nyuma.” Basi, Yoshua akaondoka, pamoja na wanajeshi wake wote kwenda Ai. Akawachagua watu hodari 30,000 na kuwaambia watangulie wakati wa usiku. Akawaamuru hivi: “Nyinyi mtauvizia mji kutoka upande wa nyuma. Msiende mbali na mji, bali muwe tayari wakati wote. Mimi, pamoja na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji. Watu watakapotoka nje kuja kutukabili kama hapo awali, sisi tutawakimbia. Nao wataendelea kutufuatia mpaka wawe mbali na mji wao, maana watafikiri wametutimua kama walivyofanya hapo awali. Sisi tutawaacha watufukuze. Hapo, nyinyi mtatokea kutoka huko mlikokuwa mnavizia na kuuteka mji, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atautia mji huo mikononi mwenu. Mkishauteka mji mtauteketeza kwa moto, kama vile Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hayo ndiyo maagizo mtakayofuata.” Basi, Yoshua akawaambia waende mahali pao pa kuvizia; nao wakajiweka magharibi ya mji wa Ai kati ya mji wa Ai na Betheli. Lakini Yoshua alilala usiku huo katika kambi ya Waisraeli. Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakusanya Waisraeli na kuelekea mjini Ai, akiwa pamoja na wazee. Wanajeshi wote waliofuatana naye walikaribia mji na kupiga kambi kaskazini yake, ngambo ya bonde mkabala wa mji wa Ai. Ndipo akachukua watu wengine 5,000 na kuwaweka wavizie kati ya mji wa Betheli na Ai, magharibi ya mji wa Ai. Kikosi kikubwa kiliwekwa kaskazini mwa mji na wale waliobaki waliwekwa magharibi ya mji. Lakini usiku huo, Yoshua akalala bondeni. Mfalme wa mji wa Ai alipoona hivyo, aliharakisha na kwenda kwenye mteremko wa kuelekea Araba ili akabiliane na Waisraeli vitani. Lakini hakujua kwamba mji wake ulikuwa umeviziwa kutoka nyuma. Kisha Yoshua pamoja na watu wake wakajifanya kana kwamba wanashindwa, wakaanza kukimbia kuelekea jangwani. Watu wote waliokuwa mjini waliitwa wawafuatie Waisraeli; na walipokuwa wanamfuatia Yoshua, walitoka na kwenda mbali na mji wao. Hakuna mtu yeyote aliyebaki mjini Ai, waliuacha mji huo wazi wakaenda kuwafuatia Waisraeli. Halafu Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Elekeza mkuki wako huko mjini Ai maana nitautia mji huo mikononi mwako.” Yoshua akaelekeza mkuki wake mjini Ai. Mara Yoshua alipouelekeza mkuki wake kule Ai, kikosi kilichokuwa kikivizia upande mwingine kikatoka na kuingia mjini; kikauteka mji na kuuteketeza kwa moto. Watu wa Ai walipotazama nyuma, wakaona moshi kutoka mjini ukipanda mpaka mbinguni. Nao hawakuwa na uwezo wa kukimbia upande wowote, maana Waisraeli waliwageukia hao waliokuwa wanawafuatia. Yoshua na Waisraeli wote walipoona kuwa kikosi kilichokuwa kinavizia kimeuteka mji, na kwamba moshi ulikuwa unapanda juu, waliwageukia na kuanza kuwaua. Watu waliobaki mjini walitoka, lakini wote wakawa wamezingirwa na Waisraeli; nao wakauawa, asibaki hata mmoja wao. Lakini mfalme wa mji wa Ai walimteka akiwa hai na kumpeleka kwa Yoshua. Waisraeli walipomaliza kabisa kuwaua watu wote wa Ai huko nyikani ambako waliwafuatia wakarudi mjini Ai na kuwaua wote waliosalia humo. Jumla ya watu wa Ai waliouawa siku hiyo, wanaume kwa wanawake, walikuwa 12,000. Yoshua hakuushusha mkono wake aliokuwa ameushikilia mkuki wake kuelekea Ai mpaka alipowaua wakazi wote wa mji huo. Waisraeli waliteka tu wanyama na mali kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Yoshua. Basi, Yoshua aliuteketeza mji wa Ai kwa moto na kuufanya magofu hadi hivi leo. Kisha akamtundika mfalme wa Ai mtini mpaka jioni. Lakini jua lilipoanza kutua, Yoshua aliamuru maiti yake iondolewe mtini na kutupwa kwenye lango la mji kisha warundike rundo kubwa la mawe juu ya maiti hiyo; rundo hilo liko huko mpaka leo. Kisha, Yoshua akamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, madhabahu mlimani Ebali, kama Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu alivyowaagiza Waisraeli, kadiri ilivyoandikwa katika kitabu cha sheria ya Mose kwamba itakuwa madhabahu iliyojengwa kwa mawe ambayo hayakuchongwa, wala kuguswa na chombo chochote cha chuma. Juu ya madhabahu hiyo walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za kuteketezwa na sadaka za amani. Na huko, mbele ya umati wote wa Waisraeli, Yoshua aliandika nakala ya sheria ya Mose juu ya mawe. Waisraeli wote pamoja na viongozi wao, wazee na waamuzi na wageni wote waliokuwa kati yao, wakasimama kila upande mkabala na sanduku la agano mbele ya makuhani Walawi waliokuwa wamelibeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Nusu yao wakasimama mbele ya mlima Gerizimu na nusu nyingine wakasimama mbele ya mlima Ebali, kama vile Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alivyoagiza hapo awali kuhusu kubarikiwa kwa Waisraeli. Kisha, Yoshua akawasomea sheria zote, pamoja na baraka na laana kama ilivyoandikwa katika kitabu cha sheria. Hakuna neno lililoamriwa na Mose ambalo Yoshua hakulisoma mbele ya umati wa Waisraeli, wakiwemo miongoni mwao wanawake, watoto na wageni. Wafalme wote waliokuwa ngambo ya mto Yordani katika nchi ya milimani na kwenye tambarare na eneo lote la pwani ya bahari ya Mediteranea kuelekea Lebanoni, Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, waliposikia habari za Waisraeli, wakakusanyika pamoja kwa nia moja ili kupigana vita na Yoshua na Waisraeli. Lakini wakazi wa Gibeoni walipopata habari juu ya jinsi Yoshua alivyoitenda miji ya Yeriko na Ai, waliamua kutumia hila. Wakatayarisha vyakula, wakapakiza magunia yaliyochakaa juu ya punda wao, viriba vilivyochakaa na kushonwa; wakavaa viatu, nguo zilizochakaa na vyakula vyao vyote vilikuwa vikavu vilivyoota ukungu. Basi, wakamwendea Yoshua kambini Gilgali, wakamwambia yeye na Waisraeli, “Sisi tumetoka nchi ya mbali; tafadhali tunaomba mfanye agano nasi.” Lakini Waisraeli wakawajibu hao Wahivi, “Tunawezaje kufanya agano nanyi? Labda nyinyi mnaishi karibu nasi.” Nao wakamwambia Yoshua, “Sisi tu watumishi wako.” Naye Yoshua akawauliza, “Nyinyi ni akina nani, na mnatoka wapi?” Wakamjibu, “Sisi, watumishi wako, tumetoka nchi ya mbali na tumekuja kwa maana tumesikia sifa za jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; tulipata habari za umaarufu wake na yote aliyoyafanya nchini Misri. Tumesikia yote aliyowatenda wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, mfalme Sihoni wa Heshboni na mfalme Ogu wa Bashani aliyekaa huko Ashtarothi. Ndipo wazee wetu na wananchi wote wa nchi yetu, wakatuambia, tuchukue posho ya safari, tuje kukutana nanyi na kuwaambia kwamba sisi ni watumishi wenu; tafadhali fanyeni agano nasi. Tazama mikate yetu ambayo ilikuwa bado moto tulipoichukua wakati tulipoondoka kwetu, lakini sasa imekauka na kuota ukungu. Viriba hivi tulivijaza maji vikiwa vipya, lakini sasa vimepasukapasuka. Hata mavazi na viatu vyetu vimechakaa, kwani safari ilikuwa ndefu sana.” Hivyo, Waisraeli wakachukua vyakula vyao, bila ya kumwuliza shauri Mwenyezi-Mungu. Yoshua akafanya nao mkataba wa amani; akafanya agano kwamba atawaruhusu kuishi. Viongozi wa jumuiya ya Israeli wakawaapia kutekeleza mapatano hayo. Siku tatu baada ya kufanya agano nao, Waisraeli wakagundua kwamba watu hao walikuwa jirani zao na waliishi miongoni mwao. Basi, Waisraeli wakafunga safari, baada ya siku ya tatu wakafika katika miji yao. Miji hiyo ilikuwa Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-yearimu. Lakini Waisraeli hawakuwaua, maana viongozi wa jumuiya ya Israeli walikuwa wamewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Hivyo basi, jumuiya yote ikawanungunikia viongozi wao. Lakini viongozi wa Waisraeli wakaiambia jumuiya ya watu wao, “Kwa vile tumewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, sasa hatuwezi kuwadhuru. Tutawaacha waishi, ili tusije tukaadhibiwa kwa sababu ya kiapo tulichokula. Waacheni waishi.” Hivyo Wagibeoni wakawa wanaitumikia jamii nzima ya Israeli, wakiwakatia kuni na kuwachotea maji, kama viongozi wa Waisraeli walivyosema. Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwauliza, “Kwa nini mlitudanganya kwamba mlitoka nchi ya mbali na hali nyinyi mnaishi miongoni mwetu? Sasa, nyinyi mmelaaniwa na baadhi yenu daima mtakuwa watumwa wa kukata kuni na kuchota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.” Wakamjibu Yoshua, “Tuliambiwa kwamba kwa hakika Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alimwamuru mtumishi wake Mose awaangamize wakazi wote wa nchi hii na kuwapa nyinyi nchi hii iwe mali yenu. Kwa hivyo, tulihofia maisha yetu na ndipo tukafanya jambo hili. Sasa sisi tumo mikononi mwako, ututendee kama unavyoona inafaa.” Basi, alilowatendea ni kuwaokoa mikononi mwa Waisraeli ili wasiangamizwe; hivyo hawakuwaua. Lakini kutoka siku hiyo, Yoshua aliwafanya hao kuwa wakata-kuni na wachota-maji kwa ajili ya jumuiya nzima ya Waisraeli na kwa ajili ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, popote pale Mwenyezi-Mungu alipochagua mpaka hivi leo. Mfalme Adoni-sedeki wa Yerusalemu alipata habari juu ya jinsi Yoshua alivyouteka mji wa Ai na kuuharibu kabisa akiutendea mji huo na mfalme wake kama alivyoutendea Yeriko na mfalme wake. Pia alipata habari kwamba wakazi wa Gibeoni walikuwa wamefanya mkataba wa amani na Waisraeli na kwamba sasa wanaishi miongoni mwao. Habari hizo zilisababisha hofu kubwa huko Yerusalemu kwa sababu mji wa Gibeoni ulikuwa maarufu miongoni mwa miji ya kifalme. Isitoshe, mji huu ulikuwa maarufu kuliko Ai na wanaume wake wote walikuwa askari hodari mno. Basi, Mfalme Adoni-sedeki akapeleka ujumbe kwa mfalme Hohamu wa Hebroni, mfalme Piramu wa Yarmuthi, mfalme Yafia wa Lakishi na mfalme Debiri wa Egloni, akawaambia, “Njoni mnisaidie tuwaangamize Wagibeoni, maana wamefanya mkataba wa amani na Yoshua pamoja na Waisraeli.” Kisha wafalme hao watano wa Waamori: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni, wakaunganisha majeshi yao, wakaenda nayo mpaka Gibeoni; wakapiga kambi kuuzingira mji huo, wakaushambulia. Wagibeoni wakapeleka ujumbe kwa Yoshua huko kambini Gilgali, wakamwambia, “Tafadhali, usitutupe sisi watumishi wako; njoo upesi utusaidie na kutuokoa kwa maana wafalme wote wa Waamori kutoka nchi ya milimani wamekuja kutushambulia.” Basi, Yoshua pamoja na jeshi lake lote na mashujaa wakaondoka Gilgali. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope hata kidogo maana nimewatia mikononi mwako, wala hakuna hata mmoja atakayeweza kukukabili.” Baada ya kutembea kutoka Gilgali usiku kucha, Yoshua akawatokea ghafla. Naye Mwenyezi-Mungu akawatia hofu kuu mbele ya Waisraeli ambao waliwaua watu wengi huko Gibeoni wakiwakimbiza kwenye njia ya mteremko wa Beth-horoni mpaka Azeka na Makeda ambako pia waliwaua watu wengi sana. Walipokuwa wakiwakimbia Waisraeli kwenye mteremko wa Beth-horoni, Mwenyezi-Mungu akawanyeshea mvua ya mawe makubwa kutoka mbinguni wakiwa njiani mpaka Azeka hata waliouawa kwa mawe hayo wakawa wengi kuliko waliouawa kwa silaha za Waisraeli. Wakati Mwenyezi-Mungu alipowatia Waamori mikononi mwa Waisraeli, Yoshua alimwomba Mwenyezi-Mungu mbele ya Waisraeli wote, akasema, “Wewe jua, simama kimya juu ya Gibeoni, wewe mwezi, katika bonde la Aiyaloni.” Jua likasimama kimya na mwezi ukasimama mpaka taifa la Israeli lilipolipiza kisasi maadui wake. Kama alivyoandika katika kitabu cha Yashari, jua lilisimama kimya katikati ya mbingu, likakatiza safari yake ya kwenda kutua kwa siku nzima. Siku kama hiyo haijawahi kuwako kamwe wala haijapata kuonekana tena, siku ambayo Mwenyezi-Mungu amemwitikia binadamu kwa namna hiyo; maana Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwapigania Waisraeli. Kisha Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Waisraeli wote. Wale wafalme watano walikimbia na kujificha katika pango la Makeda. Yoshua akapata habari kwamba wafalme hao wamegunduliwa walikojificha katika pango la Makeda. Yoshua akasema, “Vingirisheni mawe makubwa mlangoni mwa pango na kuweka walinzi hapo. Lakini nyinyi msikae huko, bali muwafuatie adui zenu. Muwapige kutoka upande wa nyuma, wala musiwaache waingie mijini mwao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu.” Yoshua pamoja na Waisraeli waliwapiga na kuwaangamiza wote, na wachache wao walionusurika walikimbilia kwenye miji yao yenye ngome. Baada ya hayo Waisraeli wote walirudi salama kwa Yoshua huko kambini Makeda; na hakuna tena mtu aliyethubutu kusema lolote dhidi ya Waisraeli. Kisha Yoshua akasema, “Fungueni mlango wa pango mniletee kutoka humo wale wafalme watano.” Wakafanya hivyo, wakamletea Yoshua wale wafalme watano: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni. Wafalme hao walipoletwa, Yoshua akawaita Waisraeli wote na wakuu wa majeshi waliokwenda naye vitani, akawaambia, “Njoni karibu mwakanyage wafalme hawa shingoni mwao.” Nao wakasogea na kuwakanyaga shingoni. Yoshua akawaambia “Msiogope, wala msiwe na wasiwasi, muwe imara na hodari, maana hivi ndivyo Mwenyezi-Mungu atakavyowatendea adui zenu ambao mtapigana nao. Kwa hiyo, muwe imara na hodari.” Baadaye, Yoshua aliwanyonga kwa kuwaangika kwenye miti mitano ambako walitundikwa mpaka jioni. Wakati jua lilipokuwa karibu kutua, Yoshua aliamuru waondolewe juu ya miti walipokuwa wameangikwa na kutupwa pangoni walimokuwa wamejificha. Kisha wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, nayo mawe hayo yako huko mpaka leo. Siku hiyo Yoshua alipouteka mji wa Makeda, alimuua mfalme wake na wakazi wake wote bila kumbakiza hata mtu mmoja. Alimtendea mfalme wa Makeda kama vile alivyomtendea mfalme wa Yeriko. Kutoka Makeda, Yoshua pamoja na Waisraeli wote walikwenda Libna wakaushambulia. Mwenyezi-Mungu akautia mji huo pamoja na mfalme wao mikononi mwa Waisraeli, wakawaua wakazi wake bila kumbakiza hata mtu mmoja. Walimtendea mfalme wa Libna kama walivyomtendea mfalme wa Yeriko. Kisha kutoka Libna Yoshua na Waisraeli wote walikwenda Lakishi, wakauzingira na kuushambulia. Naye Mwenyezi-Mungu akautia mji huo mikononi mwa Waisraeli, wakauteka mnamo siku ya pili. Waliwaua wakazi wote wa mji huo kama walivyofanya kule Libna. Hapo, mfalme Horamu wa Gerezi akaamua kuja kuwasaidia watu wa Lakishi. Lakini Yoshua alimuua pamoja na watu wake wote, hakumbakiza hata mtu mmoja. Kisha kutoka Lakishi, Yoshua na Waisraeli wote walikwenda mpaka Egloni, wakauzingira na kuushambulia. Wakauteka siku hiyohiyo na kuwaua wakazi wake wote kama walivyofanya kule Lakishi. Halafu kutoka Egloni Yoshua na Waisraeli wote wakaenda mpaka Hebroni, wakaushambulia na kuuteka. Wakawaua wakazi wake wote pamoja na mfalme wao; waliiharibu kabisa miji mingine iliyouzunguka, wakawaua wakazi wake wote kama walivyofanya kule Egloni. Kisha, Yoshua na Waisraeli wote wakarudi Debiri, wakaushambulia. Waliuteka mji huo na mfalme wake pamoja na miji mingine yote iliyouzunguka na kuwaangamiza wote waliokuwamo bila kumbakiza hata mtu mmoja. Waliutendea mji huo kama walivyoutendea mji wa Hebroni na mji wa Libna na wafalme wao. Basi, Yoshua aliiteka nchi yote; aliwashinda wafalme wa sehemu za milimani, eneo la Negebu, na sehemu za nchi tambarare na miteremko. Hakuacha chochote chenye uhai ila aliangamiza kila kitu kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alivyoamuru. Yoshua aliwashinda watu wote kutoka Kadesh-barnea mpaka Gaza, na kutoka Gosheni mpaka Gibeoni. Aliweza kuitwaa nchi hii yote kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliwapigania Waisraeli. Basi, Yoshua akarudi mpaka kambini huko Gilgali pamoja na Waisraeli wote. Mfalme Yabini wa mji wa Hazori alipopata habari hizo, alipeleka ujumbe kwa mfalme Yobabu wa Madoni, mfalme wa Shimroni na mfalme wa Akshafi, na kwa wafalme waliokuwa katika milima ya kaskazini, waliokuwa Araba ambayo ilikuwa kusini mwa Kinerethi, kwenye tambarare na waliokuwa Nafath-dori katika upande wa magharibi. Pia, alipeleka ujumbe kwa Wakanaani waliokuwa pande za mashariki na magharibi, kwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wayebusi ambao walikaa milimani na kwa Wahivi ambao walikaa chini ya mlima Hermoni katika nchi ya Mizpa. Basi, wakatoka wote na majeshi yao makubwa. Nao walikuwa wengi kama mchanga wa pwani pamoja na magari mengi na farasi wengi sana. Wafalme hawa wote wakaungana na kupiga kambi yao katika chemchemi ya Meromu ili wapigane na Waisraeli. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope hao, maana kesho, wakati kama huu, nitawaangamiza wote kwa kuwatia mikononi mwa Waisraeli; nanyi mtakata mishipa ya farasi wao na kuteketeza magari yao kwa moto.” Basi, ghafla kwenye chemchemi ya Meromu Yoshua pamoja na jeshi lake lote akawatokea na kuwashambulia. Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwa Waisraeli, nao wakawachapa na kuwafukuza mpaka Sidoni Kuu na Misrefoth-maimu, hadi upande wa mashariki katika bonde la Mizpa. Waisraeli wakawapiga na kuwaua wote. Yoshua aliwakatakata mishipa farasi wao wote na kuyateketeza magari yao kwa moto, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza. Yoshua alipokuwa anarudi, akauteka mji wa Hazori. Alimuua mfalme wake maana ndiye aliyekuwa kiongozi wa falme hizo zote. Kisha akauteketeza mji wa Hazori kwa moto na kuwaua wakazi wake wote, asimwache hata mtu mmoja. Pia aliiteketeza miji ile mingine yote kwa moto na kuwaua wafalme wao wote kama Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alivyomwamuru. Lakini Waisraeli hawakuiteketeza miji iliyokuwa vilimani, isipokuwa tu mji wa Hazori ambao Yoshua aliuteketeza. Waisraeli wakachukua vitu vyote walivyoteka nyara na wanyama wa miji hiyo; lakini waliwaua wakazi wake wote, wala hawakumwacha hata mtu mmoja. Amri hii alipewa Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, naye Mose akamwamuru Yoshua ambaye aliitekeleza. Yoshua alitimiza kila jambo Mwenyezi-Mungu alilomwamuru Mose. Yoshua aliiteka nchi nzima: Sehemu za milimani na sehemu zote za Negebu, eneo lote la Gosheni, nchi tambarare, nchi ya Araba, milima ya Israeli na sehemu zake zilizo tambarare; aliwateka na kuwaua wafalme wote wa nchi hizo kuanzia mlima uliokuwa mtupu wa Halaki karibu na Seiri mpaka Baal-gadi katika bonde la Lebanoni, kusini ya mlima Hermoni. Vita alivyopigana Yoshua na wafalme hawa wote vilichukua muda mrefu. Hakuna mji ambao ulifanya mapatano ya amani na Waisraeli, isipokuwa Gibeoni tu, ambamo waliishi Wahivi. Waisraeli waliiteka miji mingine yote kwa kupigana vita. Ilikuwa ni matakwa ya Mwenyezi-Mungu mwenyewe kuishupaza mioyo ya watu wa mataifa hayo ili wapigane. Alikusudia wasihurumiwe ila wateketezwe. Ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Wakati huo, Yoshua alikwenda, akawaangamiza Waanaki waliokuwa wanaishi katika milima huko Hebroni, Debiri, Anabu, nchi yote ya milima ya Yuda na Israeli. Yoshua aliwaangamiza watu hao pamoja na miji yao. Hakuna mtu wa kabila la Anaki ambaye alibakia katika nchi ya Israeli; walibaki wachache tu katika miji ya Gaza, Gathi na Ashdodi. Basi, Yoshua akaitwaa nchi yote kulingana na yote yale Mwenyezi-Mungu aliyomwambia Mose. Yoshua akaikabidhi kwa Waisraeli iwe mali yao, wagawane kulingana na makabila yao. Kisha nchi nzima ikatulia, ikawa haina vita tena. Wafuatao ndio wafalme ambao Waisraeli waliwashinda na kuchukua nchi yao yote iliyokuwa mashariki ya mto Yordani kutoka bonde la mto Arnoni mpaka mlima Hermoni na nchi yote ya Araba upande wa mashariki: Mfalme Sihoni wa Waamori aliyeishi huko Heshboni na kutawala kutoka makao yake makuu huko Aroeri, mji uliokuwa kandokando ya bonde la Arnoni. Alitawala pia kuanzia katikati ya bonde hadi mto Yaboki ambao ulikuwa mpaka wa nchi ya Waamoni, yaani nusu ya nchi ya Gileadi. Vilevile, alitawala nchi yote ya Araba, kutoka bahari ya Kinerethi, upande wa mashariki, mpaka Beth-yeshimothi kwenye Bahari ya Chumvi na kuendelea mpaka chini ya mlima Pisga. Mwingine ni mfalme Ogu mmoja wa Warefai waliosalia, ambaye alitawala Bashani na alikaa Ashtarothi au Edrei. Utawala wake ulienea huko kwenye mlima Hermoni, huko Saleka, Bashani yote mpaka mipaka ya Wageshuri na Wamaaka, nusu ya Gileadi hadi mpakani mwa nchi ya mfalme Sihoni wa Heshboni. Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, pamoja na Waisraeli aliwashinda wafalme hao, akayapatia nchi hizo makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase ziwe mali yao kabisa. Kisha Yoshua pamoja na Waisraeli waliwashinda wafalme wote wa eneo lote lililoko magharibi ya mto Yordani, kuanzia Baal-gadi katika bonde la Lebanoni mpaka mlima uliokuwa mtupu wa Halaki kusini karibu na Seiri. Yoshua akayagawia makabila ya Israeli nchi hizo ziwe mali yao kabisa. Nchi hizo zilikuwa pamoja na maeneo ya milima, nchi tambarare, eneo la Araba, miteremko ya milima, maeneo ya nyika, na eneo la Negebu; nchi zilizokuwa za Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Wafalme waliowashinda walikuwa, mmojammoja: Mfalme wa Yeriko, mfalme wa Ai mji ulioko karibu na Betheli, mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi, mfalme wa Egloni, mfalme wa Gezeri, mfalme wa Debiri, mfalme wa Gederi, mfalme wa Horma, mfalme wa Aradi, mfalme wa Libna, mfalme wa Adulamu, mfalme wa Makeda, mfalme wa Betheli, mfalme wa Tapua, mfalme wa Heferi, mfalme wa Afeka, mfalme wa Lasharoni, mfalme wa Madoni, mfalme wa Hazori, mfalme wa Shimron-meroni, mfalme wa Akshafi, mfalme wa Taanaki, mfalme wa Megido, mfalme wa Kedeshi, mfalme wa Yokneamu mji ulioko kwenye mlima Karmeli, mfalme wa Dori katika mkoa wa Nafath-dori, mfalme wa Goiimu huko Gilgali na mfalme wa Tirza. Jumla ya wafalme hao ni thelathini na mmoja. Wakati huu, Yoshua alikuwa mzee wa miaka mingi. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Wewe sasa umekuwa mzee wa miaka mingi, na kumebaki bado sehemu kubwa za nchi ambazo hazijatwaliwa. Sehemu hizo ni: Nchi yote ya Wafilisti na nchi yote ya Wageshuri, yaani eneo lijulikanalo kama la Wakanaani, kuanzia kijito cha Shihori mpakani mwa Misri hadi eneo la Ekroni huko kaskazini. Maeneo yote ya watawala watano wa Ufilisti: Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni pamoja na eneo la Avi, upande wa kusini. Hali kadhalika nchi za Wakanaani kuanzia Ara ya Wasidoni mpaka Afeka mpakani mwa Waamori; vilevile eneo la Gebali na Lebanoni mashariki ya Baal-gadi chini ya mlima Hermoni mpaka Lebo-hamathi; pia eneo la milima iliyo kati ya Lebanoni na Misrefoth-maimu ambayo wakazi wake ni Wasidoni. Kadiri Waisraeli watakavyoendelea katika nchi hizo, mimi mwenyewe nitayafukuza mataifa hayo mbele yao. Nawe utawagawia Waisraeli sehemu mbalimbali za nchi hizo kwa kura kama nilivyokuamuru. Utayagawia nchi hizo makabila tisa na nusu ya kabila la Manase ambayo bado hayajapata kitu.” Makabila ya Reubeni, Gadi na nusu nyingine ya kabila la Manase yalikuwa yamepewa nchi iliyo mashariki ya mto Yordani, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose, mtumishi wake. Eneo lao lilikuwa kuanzia Aroeri ukingoni mwa bonde la Arnoni na mji ule ulio katikati ya bonde, na nchi ile yote ya tambarare tangu Medeba mpaka Diboni, pamoja na miji ya mfalme Sihoni wa Waamori, aliyetawala huko Heshboni hadi mpakani mwa Waamoni, pamoja na nchi za Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaakathi, mlima wa Hermoni na nchi yote ya Bashani mpaka Saleka; na ufalme wote wa Ogu mmoja wa Warefai waliosalia, ambaye alitawala huko Ashtarothi na Edrei katika Bashani. Mose alikuwa amewashinda hao wote na kuwafukuzia mbali. Hata hivyo, Wageshuri na Wamaaka hawakufukuzwa bali wanaishi miongoni mwa Waisraeli mpaka leo. Mose hakuwapa watu wa kabila la Lawi nchi yoyote. Bali tambiko walizomtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli kwa moto, hizo ndizo zilizokuwa fungu lao, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose. Sehemu ya nchi ambayo Mose aliwapa watu wa kabila la Reubeni kulingana na jamaa zao, ilikuwa kuanzia Aroeri kando ya bonde la Arnoni na mji uliokuwa katika bonde hilo pamoja na nchi yote ya tambarare ya Medeba. Ilikuwa pia pamoja na Heshboni na miji yake yote iliyo katika sehemu tambarare: Yaani Diboni, Bamoth-baali, Beth-baal-meoni, Yahasa, Kedemothi, Mefaathi, Kiriathaimu, Sibma, Sereth-shahari, huko kilimani bondeni, Beth-peori, miteremko ya mlima Pisga, Beth-yeshimothi na miji yote ya tambarare, nchi yote ya mfalme Sihoni wa Waamori ambaye alitawala huko Heshboni; Mose alikuwa amemshinda huyu Sihoni pamoja na viongozi wa Midiani, Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba, ambao walitawala nchi kwa niaba ya mfalme Sihoni. Balaamu, mtabiri, mwana wa Beori ambaye Waisraeli walimuua alikuwa mmoja wao. Mpaka wa nchi ya kabila la Reubeni upande wa magharibi ulikuwa mto Yordani. Miji na maeneo yaliyotajwa hapa ndiyo sehemu waliyopewa watu wa koo za kabila la Reubeni. Sehemu ya nchi ambayo Mose aliwapa watu wa kabila la Gadi kulingana na koo zao ilikuwa Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Waamoni hadi Aroeri iliyo mashariki ya Raba, vilevile kuanzia Heshboni hadi Ramath-mizpe, Betonimu, na kutoka Mahanaimu mpaka wa Debiri, kadhalika miji iliyokuwa katika bonde la Beth-haramu, Beth-nimra, Sukothi na Zafoni na nchi yote iliyokuwa ya mfalme Sihoni wa Heshboni; eneo hilo lilikuwa upande wa mashariki wa Yordani na kupakana na upande wa kusini wa bahari ya Kinerethi. Miji na vijiji hivyo ndivyo walivyopewa watu wa kabila la Gadi kulingana na koo zao. Tena, Mose alikuwa ameipatia nusu ya kabila la Manase kulingana na koo zake, eneo la nchi kuanzia Mahanaimu hadi kuingia katika nchi yote iliyokuwa ya mfalme Ogu katika Bashani, pamoja na miji sitini ya Yairi, nusu ya Gileadi, Ashtarothi, Edrei, ambayo ilikuwa chini ya himaya ya mfalme Ogu wa Bashani; Eneo hili walipewa nusu ya wazawa wa Makiri mwana wa Manase, kulingana na koo zao. Mose alikuwa amewagawia sehemu hizo mbalimbali za nchi iliyokuwa mashariki ya Yeriko na Yordani, wakati alipokuwa kwenye tambarare za Moabu. Lakini kabila la Lawi, Mose hakulipa sehemu yao ya nchi, maana aliwaambia kwamba sehemu yao itakuwa kumhudumia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Yafuatayo ni maeneo ya nchi ambayo walipewa Waisraeli katika nchi ya Kanaani. Kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni, pamoja na wakuu wa koo za makabila ya Waisraeli waliwagawia Waisraeli. Sehemu yao hiyo waligawiwa kwa kura kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose awape yale makabila tisa na nusu. Mose alikuwa ameyapa yale makabila mawili na nusu sehemu yao mashariki ya Yordani, lakini Walawi hawakuwa wamepewa sehemu yao pamoja nao. Wazawa wa Yosefu walikuwa makabila mawili: Manase na Efraimu. Kabila la Lawi halikupewa sehemu yoyote ya nchi, ila miji tu ya kuishi na sehemu za malisho kwa ajili ya wanyama wao na riziki zao. Basi, Waisraeli wakaigawanya nchi kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Siku moja watu wa kabila la Yuda walimwendea Yoshua huko Gilgali. Kalebu mwana wa Yefune, ambaye alikuwa Mkenizi, akamwambia Yoshua, “Bila shaka unakumbuka jinsi Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose, mtu wa Mungu, juu yangu na wewe tulipokuwa Kadesh-barnea: Nilipokuwa na umri wa miaka arubaini, Mose mtumishi wa Mungu, alinituma kutoka Kadesh-barnea, kwenda kuipeleleza nchi. Niliporudi nilimletea habari za mambo ya huko kadiri nilivyoamini moyoni mwangu, hali wale wenzangu waliokwenda pamoja nami waliwavunja watu moyo, lakini mimi nilimfuata Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kwa uaminifu. Siku hiyo Mose aliniapia, ‘Hakika sehemu ya nchi ile ambayo ulipita itakuwa yako wewe na wazawa wako milele. Kwa sababu ya uaminifu wako kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako’. Lakini sasa tazama! Ni muda wa miaka arubaini na mitano tangu Mwenyezi-Mungu alipoongea na Mose, wakati Waisraeli walipokuwa wanapitia jangwani. Tangu wakati huo Mwenyezi-Mungu, kama alivyoahidi, amenihifadhi hai mpaka leo, na sasa mimi nina umri wa miaka themanini na mitano. Lakini bado nina nguvu kama nilivyokuwa wakati ule Mose aliponituma. Hata sasa nina nguvu za kuweza kupigana vita au kufanya kazi nyingine yoyote. Sasa naomba unipe nchi hii ya milima ambayo Mwenyezi-Mungu aliniahidi siku ile. Wewe ulisikia siku ile kwamba Waanaki waliishi humo katika miji yenye ngome; huenda Mwenyezi-Mungu atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.” Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune na kumpa mji wa Hebroni kuwa sehemu yake. Kwa hiyo, mji wa Hebroni ni sehemu yao wazawa wa Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi mpaka hivi leo, kwa sababu Kalebu alikuwa mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Mji wa Hebroni hapo awali uliitwa Kiriath-arba. Arba alikuwa mtu maarufu kuliko wote kati ya Waanaki. Nchi nzima ikawa tulivu bila vita. Eneo la nchi waliyopewa kwa kura watu wa kabila la Yuda kulingana na jamaa zake lilienea tangu kusini-mashariki hadi mpakani mwa Edomu. Sehemu ya kusini kabisa ilikuwa jangwa la Sini. Mpaka wao upande wa kusini ulianza pembe ya kusini ya Bahari ya Chumvi, ukaendelea kusini hadi mwinuko wa Akrabimu, ukapitia kando ya Sini, na kusini ya Kadesh-barnea, ukipitia Hesroni hadi Adari na kisha ukageuka kuelekea Karka. Kutoka hapo ulipita karibu na Asmoni na kufuata kijito cha Misri hadi kufikia kwenye bahari ya Mediteranea. Hapo ndipo ulipopita mpaka wa kusini wa Yuda. Mpaka wao wa upande wa mashariki ni Bahari ya Chumvi hadi pale mto Yordani unapoingilia baharini. Na mpaka wao upande wa kaskazini ulipita kutoka pembe ya Bahari ya Chumvi mahali ambapo mto Yordani unaingilia baharini. Mpaka huo ukapita Bethi-hogla na kaskazini ya Beth-araba hadi kwenye jiwe la Bohani mwana wa Reubeni. Kutoka hapo, uliendelea hadi Debiri kwenye bonde la Akori na kaskazini kuelekea Gilgali, ulio karibu na mwinuko wa Adumimu ambao uko kusini mwa kijito, kisha ukaelekea kwenye chemchemi za En-shemeshi na kuishia En-rogeli. Kisha, mpaka huo ulipitia kwenye Bonde la Hinomu, upande wa kusini mwa kilima cha Wayebusi, yaani Yerusalemu, kuelekea kilele cha mlima ulio magharibi ya bonde la Hinomu na kufika mwishoni mwa bonde la Refaimu. Kutoka hapo, ulielekea mlimani hadi chemchemi za Neftoa, mpaka kwenye miji ya mlima wa Efroni. Hapo mpaka uligeuka na kuelekea Baala, yaani Kiriath-yearimu, ambako ulipinda magharibi kuelekea Mlima Seiri; ukapita kaskazini ya mlima wa Yerimu, yaani Kesaloni, na kuteremka hadi Beth-shemeshi ambapo ulipita karibu na Timna. Kisha ukaendelea upande wa kaskazini wa Ekroni, ukazunguka kuelekea Shikroni ambapo ulipita karibu na mlima Baala hadi Yabneeli ukaishia katika bahari ya Mediteranea. Mpaka wa magharibi ulikuwa bahari ya Mediteranea. Ndivyo ilivyokuwa mipaka ya eneo walilopewa watu wa kabila la Yuda kulingana na koo zao. Kalebu mwana wa Yefune, alipewa sehemu ya nchi ya Yuda kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Yoshua. Alipewa Kiriath-arba au mji wa Arba ambaye alikuwa babu wa Anaki. Mji huo sasa unaitwa Hebroni. Kalebu alizifukuza kutoka mji huo koo tatu za Anaki yaani ukoo wa Sheshai, ukoo wa Ahimani na ukoo wa Talmai. Kutoka Hebroni alikwenda kuwashambulia wakazi wa Debiri, mji ambao hapo awali uliitwa Kiriath-seferi. Kalebu akatangaza kwamba atamwoza binti yake Aksa kwa mwanamume yeyote atakayeuteka mji wa Kiriath-seferi. Basi, Othnieli, mwana wa Kenazi, nduguye Kalebu, akauteka mji huo, naye Kalebu akamwoza bintiye. Katika siku yao ya harusi, Aksa alimwambia Othnieli amwombe Kalebu shamba. Aksa alikuwa amepanda punda, na alipokuwa anashuka chini, Kalebu akamwuliza, “Unataka nikupe nini?” Aksa akamjibu, “Nipe zawadi; nipe sehemu yenye maji kwa kuwa huko Negebu ulikonipa ni kukavu.” Basi, Kalebu akampa chemchemi za maji zilizokuwa kwenye nyanda za juu na za chini. Hii ndiyo nchi waliyopewa watu wa kabila la Yuda kulingana na koo zake. Miji iliyokuwa upande wa kusini kabisa wa nchi ya Yuda kuelekea mpaka wa Edomu ilikuwa: Kabseeli, Ederi, Yaguri, Kina, Dimona, Adada, Kedeshi, Hazori, Ithnani, Zifu, Telemu, Bealothi, Hazor-hadata, Kerioth-hezroni (yaani Hazori), Amamu, Shema, Molada, Hasar-gada, Heshmoni, Beth-peleti, Hasar-shuali, Beer-sheba, Biziothia, Baala, Iyimu, Ezemu, Eltoladi, Kesili, Horma, Siklagi, Madmana, Sansana, Lebaothi, Shilhimu, Aini na Rimoni. Jumla ya miji waliyopewa ni ishirini na tisa pamoja na vijiji vyake. Miji iliyokuwa kwenye tambarare ilikuwa: Eshtaoli, Sora, Ashna, Zanoa, Enganimu, Tapua, Enamu, Yarmuthi, Adulamu, Soko, Azeka, Shaaraimu, Adithaimu, Gedera na Gederothaimu. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na minne pamoja na vijiji vyake. Walipewa pia miji ya Senani, Hadasha, Migdal-gadi, Dileani, Mizpa, Yoktheeli, Lakishi, Boskathi, Egloni, Kaboni, Lahmamu, Kithlishi, Gederothi, Beth-dagoni, Naama na Makeda. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na sita pamoja na vijiji vyake. Tena walipewa miji ya Libna, Etheri, Ashani, Yifta, Ashna, Nezibu, Keila, Akzibu na Maresha. Jumla ya miji waliyopewa ni tisa pamoja na vijiji vyake. Vilevile walipewa Ekroni pamoja na miji yake midogo na vijiji, miji yote na vijiji vilivyokuwa karibu na Ashdodi kati ya Ekroni na bahari, Ashdodi na Gaza pamoja na miji na vijiji vyake, mpaka kijito cha Misri hadi pwani ya bahari ya Mediteranea. Miji iliyokuwa kwenye eneo la milimani ni Shamiri, Yatiri, Soko, Dana, Kiriath-sana (yaani Debiri), Anabu, Eshtemoa, Animu, Gosheni, Holoni na Gilo. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na mmoja pamoja na vijiji vyake. Walipewa pia miji ya Arabu, Duma, Eshani, Yanimu, Beth-tapua, Afeka, Humta, Kiriath-arba (yaani Hebroni) na Siori. Jumla ya miji waliyopewa ni tisa pamoja na vijiji vyake. Pia walipewa miji ya Maoni, Karmeli, Zifu, Yuta, Yezreeli, Yokdeamu, Zanoa, Kaini, Gibea na Timna. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi pamoja na vijiji vyake. Vilevile miji ya Halhuli, Beth-suri, Gedori, Maarathi, Beth-anothi na Eltekoni. Jumla ya miji waliyopewa ni sita pamoja na vijiji vyake. Kadhalika walipewa Kiriath-baali, uitwao pia Kiriath-yearimu, na Raba. Jumla ya miji waliyopewa ni miwili pamoja na vijiji vyake. Miji ya nyikani ilikuwa Beth-araba, Midini, Sekaka, Nibshani, Mji wa Chumvi na Engedi. Jumla ya miji waliyopewa ni sita pamoja na vijiji vyake. Lakini watu wa Yuda hawakuweza kuwafukuza Wayebusi, ambao ndio waliokuwa wenyeji wa Yerusalemu, na mpaka leo Wayebusi bado wanaishi mjini humo pamoja na watu wa Yuda. Sehemu waliyogawiwa wazawa wa Yosefu kwa kura ilianzia karibu na mto Yordani, mashariki ya chemchemi ya Yeriko, na kupitia jangwani, hadi kwenye sehemu za milima mpaka Betheli. Kutoka Betheli mpaka ulielekea Luzu ukapita Atarothi ambako waliishi Waarki. Kisha ukashuka magharibi katika nchi ya Wayafleti hadi Beth-horoni ya Chini na Gezeri na kuishia kwenye bahari ya Mediteranea. Wazawa wa Yosefu, yaani kabila la Manase na kabila la Efraimu, walipewa nchi hiyo kuwa milki yao. Watu wa kabila la Efraimu kulingana na jamaa zao walipata sehemu yao ambayo mpaka wake upande wa mashariki ulipita Ataroth-adari hadi Beth-horoni ya Juu, na kuishia bahari ya Mediteranea. Kwa upande wa kaskazini mpaka ulipita Mikmethathi na kwa mashariki yake ulizunguka na kuelekea Taanath-shilo ambako ulipita upande wa mashariki hadi Yanoa. Kutoka Yanoa ulikwenda hadi Atarothi na Naara, hata kufika Yeriko, ambako uliishia katika mto Yordani. Kutoka Tapua, mpaka ulikwenda magharibi hadi kijito cha Kana na kuishia bahari ya Mediteranea. Hii ndiyo nchi waliyopewa watu wa kabila la Efraimu kulingana na jamaa zao, pamoja na miji na vijiji ambavyo waliongezewa kutoka kwenye nchi ya kabila la Manase. Waefraimu hawakuwafukuza Wakanaani walioishi Gezeri. Wakanaani hao waliendelea kukaa miongoni mwa watu wa Efraimu mpaka leo, wakiwa watumwa wa kuwafanyia kazi za kulazimishwa. Watu wa kabila la Manase ambaye alikuwa mzaliwa wa kwanza wa Yosefu, pia walipewa eneo lao kwa kura. Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase na baba yake Gileadi, alikwishapewa kwa kura miji ya Gileadi na Bashani, maana alikuwa hodari vitani. Wengine waliobaki wa kabila la Manase walipewa sehemu yao kwa kura kulingana na koo zao. Koo hizo zilikuwa zile za Abiezeri, Heleki, Asrieli, Shekemu, Heferi na Shemida ambao wote walikuwa wazawa wa kiume wa Manase mwana wa Yosefu. Lakini Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na watoto wa kiume, bali alikuwa na watoto wa kike tu, nao walikuwa: Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirza. Mabinti hao wakamjia kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni, na viongozi wengine wakawaambia, “Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose atugawie na sisi sote nchi kama wagawiwavyo wanaume wa kabila letu.” Basi kufuatana na amri ya Mwenyezi-Mungu, Yoshua akawapatia sehemu yao kama alivyowapa wanaume wa kabila lao. Kwa hiyo kabila la Manase liliongezewa sehemu mbili zaidi yaani nchi ya Gileadi na Bashani iliyoko upande mwingine wa mto Yordani, kwa sababu binti za Manase waligawiwa sehemu zao kama walivyogawiwa wanaume wa kabila lao. (Nchi ya Gileadi walipewa wazawa wengine wa Manase). Eneo la kabila la Manase lilianzia Asheri na kwenda hadi Mikmethathi mashariki ya Shekemu; halafu mpaka wao ukaendelea kusini hadi kwenye nchi ya wakazi wa En-tapua. Nchi ya Tapua ilikuwa mali yake Manase, lakini mji wa Tapua, ambao ulikuwa mpakani, ulikuwa mali ya wazawa wa Efraimu. Mpaka huo uliendelea hadi kijito cha Kana. Miji iliyokuwa kusini ya Kana ilikuwa ya Waefraimu hata ingawa ilikuwa katika nchi ya kabila la Manase. Halafu mpaka ukapita kaskazini ya kijito Kana na kuishia bahari ya Mediteranea. Eneo la kusini lilikuwa la kabila la Efraimu na eneo la kaskazini lilikuwa la kabila la Manase, mpaka wake ukiwa bahari ya Mediteranea kwa upande wa magharibi. Kabila la Asheri lilikuwa kaskazini-magharibi ya eneo la Manase na kaskazini-mashariki lilikuwa kabila la Isakari. Vilevile katika nchi ya kabila la Isakari na kabila la Asheri, kabila la Manase lilipatiwa miji ya Beth-sheani na Ibleamu pamoja na vijiji vyake, na miji ya Dori, En-dori, Taanaki na Megido pamoja na wakazi na vijiji vyake; na pia theluthi ya Nafathi. Lakini wazawa wa Manase hawakuweza kuwafukuza wakazi wa miji hiyo, Wakanaani wakaendelea kuishi humo, ingawa hata baada ya Waisraeli kuwa na nguvu zaidi, hawakuweza kuwafukuza ila tu waliwafanyisha kazi za kulazimishwa. Watu wa kabila la Yosefu walimwendea Yoshua, wakamwambia, “Kwa nini umetugawia sehemu moja tu ya nchi sisi ambao Mwenyezi-Mungu ametubariki hata akatufanya tuwe wengi sana?” Yoshua akawajibu, “Kama mmekuwa wengi hivyo, hata nchi ya milima ya Efraimu haiwatoshi tena, basi nendeni msituni katika nchi ya Waperizi na ya Warefai, mkaufyeke msitu huo na kufanya makao yenu huko.” Nao wakamjibu, “Ni kweli kwamba nchi hii ya milima haitutoshi; hata hivyo wale Wakanaani wote wanaokaa kwenye tambarare wana magari ya chuma, vilevile wale wote wanaokaa Beth-sheani pamoja na vijiji vyake, na wale wanaoishi katika Bonde la Yezreeli.” Basi, Yoshua akawaambia wazawa wa Yosefu, yaani kabila la Efraimu na Manase, “Kweli nyinyi mmekuwa wengi na wenye uwezo mkubwa. Haifai mpate sehemu moja tu, bali pia nchi ya milima itakuwa yenu. Ingawa sasa ni msitu, mtaifyeka na kuimiliki yote toka upande huu hadi upande mwingine. Mtawaondoa Wakanaani, hata kama wana magari ya chuma na ni wenye nguvu.” Baada ya kuishinda ile nchi, jumuiya yote ya Waisraeli ilikusanyika huko Shilo na kulisimika hema la mkutano. Yalikuwa yamebaki kati yao makabila saba ambayo hayakuwa yamegawiwa sehemu yao ya nchi. Kwa hiyo, Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtakawia mpaka lini kwenda kuimiliki nchi ile ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, amewapeni? Chagueni watu watatu kutoka kila kabila niwatume nchini kote wachunguze na kuchora ramani kulingana na makabila yao, kisha waniletee taarifa. Nao wataigawanya nchi hiyo sehemu saba. Kabila la Yuda litabaki na sehemu yake ya kusini na kabila la Yosefu kaskazini. Tayarisheni maelezo kamili juu ya sehemu zote saba na kuniletea. Hapo, nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kuhusu sehemu ya kila kabila lenu. Lakini Walawi hawatapata sehemu yoyote kati yenu, maana sehemu yao ni kuwa makuhani wa kumhudumia Mwenyezi-Mungu. Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase walikwisha pata sehemu yao upande wa mashariki wa mto Yordani. Walipewa sehemu hii na Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu.” Basi, watu hao wakaanza safari ya kwenda kuichunguza nchi. Kabla hawajaenda, Yoshua akawapa maagizo: “Nendeni nchini kote mkaandike maelezo kamili juu ya hiyo nchi, kisha mrudi mnieleze, nami nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu hapa hapa Shilo kuhusu sehemu mtakayopewa.” Wanaume hao wakazunguka nchini kote, wakachora maelezo kamili juu ya sehemu zake saba pamoja na miji yake, kisha wakarudi kwa Yoshua kule kambini Shilo. Huko Shilo, Yoshua akazipigia kura sehemu hizo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawagawia Waisraeli; kila kabila na sehemu yake. Kura ya kwanza ililipata kabila la Benyamini kulingana na koo zake. Eneo walilopewa watu hao lilikuwa katikati ya lile la kabila la Yuda na lile la kabila la Yosefu. Mpaka wake wa kaskazini ulianzia mto Yordani na kupitia kaskazini mwa Yeriko na nchi ya milima ukaelekea magharibi hadi kwenye nyika ya Beth-aveni. Kutoka huko, mpaka wake ulikwenda kusini kuelekea Luzu kupitia upande wa kusini wa Luzu (yaani Betheli) hadi Ataroth-adari, kwenye mlima ulioko kusini mwa Beth-horoni ya Chini. Upande wa magharibi wa mlima huo ulio kusini mwa Beth-horoni mpaka uligeuka ukaelekea kusini hadi Kiriath-baali, uitwao pia Kiriath-yearimu, mji ambao ni mali ya kabila la Yuda. Huu ndio uliokuwa mpaka wake upande wa magharibi. Upande wa kusini mpaka wake ulianzia kwenye viunga vya mji wa Kiriath-yearimu, ukafika Efroni na kwenda hadi kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa. Kisha ulielekea chini kupitia pembeni mwa mlima ulioko karibu na bonde la mwana wa Hinomu, ambalo lilikuwa katika sehemu ya kaskazini zaidi ya bonde la Warefai. Halafu mpaka uliteremka kuelekea bonde la Hinomu, kusini mwa kilima cha Wayebusi, ukaendelea kuteremka hadi En-rogeli. Huko, mpaka uligeuka kwenda kaskazini kuelekea En-shemeshi, ukapitia Gelilothi unaokabili mwinuko wa Adumimu na kuteremka hadi kwenye jiwe la Bohani mwana wa Reubeni. Kutoka hapo, mpaka ulizunguka kaskazini kwenye ukingo wa juu wa Araba na kuishia huko Araba. Tena, ukaendelea kwa upande wa kaskazini wa kilima cha Beth-hogla na kuishia kaskazini kabisa ya ghuba ya Bahari ya Chumvi, mahali unapoingilia mto Yordani. Huu ni mpaka wake kwa upande wa kusini. Mto Yordani ndio uliokuwa mpaka wake upande wa mashariki. Ndivyo zilivyowekewa mipaka nchi zilizopewa koo za kabila la Benyamini. Miji ya koo za kabila la Benyamini ni Yeriko, Beth-hogla, Emek-kesisi, Beth-araba, Zemaraimu, Betheli, Avimu, Para, Ofra, Kefar-amoni, Ofni na Geba. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na miwili pamoja na vijiji vyake. Miji mingine ni Gibeoni, Rama, Beerothi, Mizpa, Kefira, Moza, Rekemu, Irpeeli, Tarala, Zela, Ha-elefu, Yebusi, yaani Yerusalemu, Gibea na Kiriath-yearimu. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na minne pamoja na vijiji vyake. Hiyo yote ni sehemu waliyopewa watu wa kabila la Benyamini na koo zao. Kura ya pili ilizipata koo za kabila la Simeoni na sehemu yao ya nchi ilikuwa imezungukwa na ile ya kabila la Yuda. Kabila la Simeoni lilipata miji ya Beer-sheba, Sheba, Molada Hasar-shuali, Bala, Esemu, Eltoladi, Bethuli, Horma, Siklagi, Beth-markabothi, Hasar-susa, Beth-lebaothi na Sharuheni. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na mitatu pamoja na vijiji vyake. Pia kulikuwa na miji ya En-rimoni, Etheri, na Ashani. Jumla ya miji waliyopewa ni minne pamoja na vijiji vyake. Pamoja na vijiji vyote vilivyoizunguka miji hiyo hadi Baalath-beeri, (au Rama) ya Negebu. Hizo zote ni sehemu zilizopewa koo za kabila la Simeoni. Kwa vile eneo lililopewa kabila la Yuda lilikuwa kubwa kuliko kabila hilo lilivyohitaji, sehemu ya eneo lake lilipewa kabila la Simeoni. Kura ya tatu ilizipata koo za kabila la Zebuluni. Eneo lao lilienea hadi Saridi. Kutoka huko mpaka wake ulikwenda magharibi hadi Mareali, ukapitia pembeni mwa Dabeshethi na kwenda kwenye kijito kilichoko mashariki ya Yokneamu. Kutoka Saridi, mpaka huo ulielekea mashariki hadi kwenye mpaka wa Kisloth-tabori, na kutoka huko ukapita Daberathi hadi Yafia. Kutoka Yafia uliendelea mashariki hadi Gath-heferi, Eth-kasini, na kuendelea hadi Rimoni ambako ulipanda kuelekea Nea. Upande wa kaskazini mpaka uligeuka kuelekea Hanathoni na kuishia kwenye bonde la Yiftaheli. Ukajumuisha miji ya Katathi, Nahalali, Shimroni, Yidala na Bethlehemu. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na miwili pamoja na vijiji vyake. Hiyo ndiyo sehemu zilizopewa koo za kabila la Zebuluni miji hiyo pamoja na vijiji vyake. Kura ya nne ilizipata koo za kabila la Isakari. Eneo lenyewe lilikuwa na miji ya Yezreeli, Kesulothi, Shunemu, Hafaraimu, Shioni, Anaharathi, Rabithi, Kishioni, Ebesi, Remethi, En-ganimu, En-hada na Beth-pasesi. Kadhalika, mpaka wao ulifika Tabori, Shahasuma, Beth-shemeshi na kuishia kwenye mto Yordani. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na sita pamoja na vijiji vyake. Hizo ndizo sehemu zilizopewa koo za kabila la Isakari; miji hiyo pamoja na vijiji vyake. Kura ya tano ilizipata koo za kabila la Asheri. Eneo la nchi yao lilikuwa na miji ya Helkathi, Hali, Beteni, Akshafi, Alameleki, Amadi na Mishali. Kwa upande wa magharibi mpaka uligusana na Karmeli na Shihor-libnathi. Kisha ukageuka kuelekea mashariki kwenda Beth-dagoni ambako unagusana na Zebuluni na bonde la Iftaheli. Halafu ukaendelea kaskazini hadi Beth-emeki, Neieli na kuzidi kuelekea kaskazini hadi Kabuli, Ebroni, Rehobu, Hamoni, Kana hadi Sidoni Kuu. Hapo, mpaka uligeuka kuelekea Rama na kufikia kwenye mji wa Tiro uliokuwa na ngome. Kisha ukageuka kuelekea Hosa na kuishia kwenye bahari ya Mediteranea. Miji mingine iliyokuwamo ni Maharabu, Akzibu, Uma, Afeka na Rehobu. Jumla ya miji waliyopewa ni ishirini na miwili pamoja na vijiji vyake. Sehemu hizo ndizo zilizopewa koo za kabila la Asheri; miji hiyo pamoja na vijiji vyake. Kura ya sita ilizipata koo za kabila la Naftali. Mpaka wake ulianzia Helefu na mwaloni mwa Zaananimu, ukapita Adami-nekebu na Yabneeli hadi Lakumu na kuishia kwenye mto Yordani. Kutoka hapo mpaka ulikwenda magharibi kuelekea Aznoth-tabori; toka huko ukaenda Hukoki na kugusana na pembe ya kusini ya eneo la kabila la Zebuluni; kisha kugusana na eneo la kabila la Asheri upande wa magharibi, na kugusana na eneo la kabila la Yuda. Kwa upande wa mashariki mpaka ukiingilia kwenye mto Yordani. Miji yao iliyokuwa na ngome ni Zidimu, Zeri, Hamathi, Rakathi, Kinerethi, Adama, Rama, Hazori, Kedeshi, Edrei, En-hazori, Yironi, Migdaleli, Horemu, Beth-anathi na Beth-shemeshi. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na tisa pamoja na vijiji vyake. Hizo ndizo sehemu zilizopewa koo za kabila la Naftali; miji hiyo pamoja na vijiji vyake. Kura ya saba ilizipata koo za kabila la Dani. Eneo la nchi yao lilikuwa na miji ya Sora, Eshtaoli, Ir-shemeshi Shaalabini, Aiyaloni, Yithla, Eloni, Timna, Ekroni Elteke, Gibethoni, Baalathi, Yehudi, Bene-beraki, Gath-rimoni, Me-yarkoni na Rakoni na nchi iliyokuwa karibu na Yopa. Watu wa kabila la Dani walipopoteza nchi yao, walikwenda na kuushambulia mji wa Leshemu. Waliushinda na kuuteka, na baada ya kuwaua wakazi wake wote, waliumiliki halafu wakabadili jina la mji huo kuwa Dani; jina ambalo lilikuwa ni la babu yao. Hizo ndizo sehemu zilizopewa koo za kabila la Dani; miji hiyo pamoja na vijiji vyake. Walipomaliza kugawiana sehemu zote za nchi, Waisraeli walimpa Yoshua, mwana wa Nuni, sehemu yake katikati yao. Kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu walimpa mji ambao aliuchagua yeye mwenyewe, yaani Timnath-sera, ambao ulikuwa katika nchi ya milima ya Efraimu. Naye Yoshua akaujenga upya mji huo na kukaa humo. Basi, kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni, pamoja na viongozi wa makabila ya Waisraeli waligawa sehemu hizo kwa kura mbele ya Mwenyezi-Mungu mlangoni mwa hema la mkutano huko Shilo. Basi, wakakamilisha kuigawa nchi. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, awaambie Waisraeli hivi: “Jichagulieni miji ambamo mtu aweza kukimbilia usalama ambayo nilimwambia Mose akueleze. Mtu yeyote akimuua mtu bila kukusudia anaweza kukimbilia katika mji mmojawapo na hivyo kumkwepa yule mtu aliye na jukumu la kulipiza kisasi cha damu. Mwuaji atakimbilia katika mji mmojawapo na kusimama mlangoni mwa mji na kuwaeleza wazee wa mji huo kesi yake. Wazee watampokea ndani na kumpa mahali pa kuishi pamoja nao. Yule mwenye kulipiza kisasi akimwandama mpaka mjini, wazee wa mji huo hawaruhusiwi kumtoa mwuaji huyo kwa yule mwenye kulipiza kisasi, maana alimuua mwenzake kwa bahati mbaya, kwa vile hapakuwa na uadui kati yao hapo awali. Mwuaji ataendelea kuishi humo mpaka hapo atakapohukumiwa mbele ya jumuiya nzima ya Israeli na pia mpaka hapo yule kuhani mkuu ambaye alikuwa na madaraka wakati huo amefariki. Baada ya hapo mtu huyo ataweza kurudi nyumbani kwake katika mji ule alikotoroka.” Basi, kwa ajili hiyo wakaitenga miji ya Kedeshi katika Galilaya kwenye milima ya Naftali, Shekemu katika milima ya Efraimu na Kiriath-arba (yaani Hebroni) katika nchi ya milima ya Yuda. Katika ngambo ya mto Yordani, mashariki ya mji wa Yeriko, walichagua mji wa Bezeri ulio kwenye nyika tambarare na ambao mji wenyewe ni wa eneo la kabila la Reubeni. Pia walichagua Ramothi huko Gileadi ambao ni mji wa kabila la Gadi na Golani huko Bashani katika eneo la kabila la Manase. Hii ndiyo miji iliyotengwa kwa ajili ya watu wote wa Israeli na wageni walioishi miongoni mwao, ili mtu yeyote atakayemuua mwenzake bila kukusudia akimbilie huko asije akauawa na mwenye jukumu la kulipiza kisasi cha damu, hadi hapo atakapohukumiwa mbele ya jumuiya nzima. Walipokuwa huko Shilo katika nchi ya Kanaani viongozi wa koo za Walawi wakawaendea kuhani Eleazari na Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa za makabila yote ya Waisraeli, wakawaambia, “Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose tupewe miji ya kuishi na mbuga za malisho ya wanyama wetu.” Basi, kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu, Waisraeli walichagua kutoka katika maeneo ya nchi zao, miji na vijiji vya malisho, wakawapa Walawi iwe sehemu yao. Kura ya kwanza ilizipata jamaa za ukoo wa Kohathi. Miongoni mwao wazawa wa kuhani Aroni walipewa kwa kura, miji iliyokuwa katika maeneo ya makabila ya Yuda, Simeoni, na Benyamini. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na mitatu. Watu wa ukoo wa Kohathi waliosalia walipewa miji kumi iliyoko katika maeneo ya makabila ya Efraimu, Dani na katika eneo la nusu ya kabila la Manase. Watu wa ukoo wa Gershoni walipewa kwa kura miji kumi na mitatu katika maeneo ya makabila ya Isakari, Asheri, Naftali na katika eneo la nusu ya kabila la Manase huko Bashani. Jamaa za ukoo wa Merari walipewa miji kumi na miwili katika maeneo ya makabila ya Reubeni, Gadi na Zebuluni. Waisraeli waliwapa Walawi miji hiyo pamoja na vijiji vya malisho yao, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza Mose. Yafuatayo ni majina ya miji kutoka kwenye maeneo ya kabila la Yuda na Simeoni ambayo ilitolewa kwa wazawa wa kuhani Aroni, waliokuwa jamaa za ukoo wa Kohathi ambaye alikuwa wa kabila la Lawi. Sehemu yao walipata kwanza kwani kura yao ilitokea kwanza. Walipewa Kiriath-arba yaani Hebroni (Arba alikuwa baba yake Anaki) katika milima ya Yuda, pamoja na mbuga zilizoizunguka. Lakini mashamba ya mji huo pamoja na vijiji vilivyouzunguka alikuwa amekwisha pewa Kalebu mwana wa Yefune viwe mali yake. Licha ya kuwapa wazawa wa kuhani Aroni mji wa Hebroni ambao pia ulikuwa umetengwa kuwa mji wa kukimbilia usalama, waliwapa miji ya Libna pamoja na mbuga zake za malisho, Yatiri pamoja na mbuga zake za malisho, Eshtemoa pamoja na mbuga zake za malisho, Holoni pamoja na mbuga zake za malisho, Debiri pamoja na mbuga zake za malisho, Aini pamoja na mbuga zake za malisho, Yuta pamoja na mbuga zake za malisho na Beth-shemeshi pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji hiyo iliyo katika maeneo ya makabila hayo mawili ni tisa. Katika eneo la kabila la Benyamini walipewa miji mingine: Gibeoni pamoja na mbuga zake za malisho, Anathothi pamoja na mbuga zake za malisho, Almoni pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. Miji yote ya wazawa wa Aroni ambao walikuwa makuhani, ilikuwa kumi na mitatu pamoja na mbuga zao za malisho. Watu waliosalia wa ukoo wa Kohathi, ambao pia ni jamaa za kabila la Lawi walipewa miji katika eneo la kabila la Efraimu. Walipewa Shekemu, mji ambao ulikuwa pia mji wa kukimbilia usalama, pamoja na mbuga zake za malisho katika nchi ya milima ya Efraimu, na Gezeri pamoja na mbuga zake za malisho, Kibzaimu pamoja na mbuga zake za malisho na Beth-horoni pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. Katika eneo la kabila la Dani walipewa Elteke pamoja na mbuga zake za malisho, Gibethoni pamoja na mbuga zake za malisho, Aiyaloni pamoja na mbuga zake za malisho na Gath-rimoni pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. Katika eneo la nusu ya kabila la Manase walipewa Taanaki pamoja na mbuga zake za malisho na Gath-rimoni pamoja na malisho yake. Jumla ya miji waliyopewa ni miwili. Basi, miji ambayo walipewa jamaa za Kohathi zilizosalia ilikuwa kumi pamoja na mbuga zao za malisho. Jamaa za Walawi za ukoo wa Gershoni, walipewa miji miwili katika nusu ya eneo la kabila la Manase: Golani, huko Bashani, mji wa kukimbilia usalama, pamoja na mbuga zake za malisho, na Beesh-tera pamoja na malisho yake. Katika eneo la kabila la Isakari, walipewa Kishioni pamoja na mbuga zake za malisho, Daberathi pamoja na mbuga zake za malisho, Yarmuthi pamoja na mbuga zake za malisho na En-ganimu pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. Katika eneo la kabila la Asheri walipewa Mishali pamoja na mbuga zake za malisho, Abdoni pamoja na mbuga zake za malisho, Helkathi pamoja na mbuga zake za malisho na Rehobu pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. Katika eneo la kabila la Naftali walipewa Kedeshi, mji wa kukimbilia usalama ulioko huko Galilaya pamoja na mbuga zake za malisho, Hamoth-dori pamoja na mbuga zake za malisho na Kartani pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla miji mitatu. Jumla ya miji ya jamaa mbalimbali za ukoo wa Gershoni ilikuwa kumi na mitatu pamoja na mbuga zao za malisho. Walawi wengine waliobaki, yaani wazawa wa Merari, walipewa miji katika eneo la kabila la Zebuluni. Nayo ni Yokneamu pamoja na mbuga zake za malisho, Karta pamoja na mbuga zake za malisho, Dimna pamoja na mbuga zake za malisho na Nahalali pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla miji minne. Katika eneo la kabila la Reubeni walipewa Bezeri pamoja na mbuga zake za malisho, Yahazi pamoja na mbuga zake za malisho, Kedemothi pamoja na mbuga zake za malisho na Mefaathi pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla miji minne. Katika eneo la kabila la Gadi walipewa Ramothi wa Gileadi, mji wa kukimbilia usalama, pamoja na mbuga zake za malisho, Mahanaimu pamoja na mbuga zake za malisho, Heshboni pamoja na mbuga zake za malisho na Yazeri pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla miji minne. Miji yote waliyopewa wazawa wa Merari, yaani jamaa za Walawi zilizobaki, ilikuwa kumi na miwili. Jumla ya miji yote ambayo Walawi walipewa katika maeneo ya Waisraeli ilikuwa arubaini na minane pamoja na mbuga zao za malisho. Kila mmoja kati ya miji hii ulizungukwa na mbuga za malisho. Basi, Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli nchi yote ambayo alikuwa amewaahidi wazee wao. Nao wakaimiliki na kuishi humo. Mwenyezi-Mungu akawapa amani kila mahali nchini kama alivyowaapia wazee wao. Hakuna adui yeyote aliyethubutu kuwakabili kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa amewatia adui hao mikononi mwao. Hakuna hata ahadi yoyote njema ambayo Mwenyezi-Mungu aliiahidi Israeli ambayo haikutimia. Ahadi zote zilitimia. Basi, Yoshua akawaita watu wa kabila la Reubeni, la Gadi na watu wa nusu ya kabila la Manase akawaambia, “Nyinyi mmefuata yale yote Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliyowaamuru na mmetii maagizo niliyowaamuru. Wala hamkuwaacha ndugu zenu muda huo wote mrefu mpaka leo, bali mmefuata kwa makini amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Sasa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapa ndugu zenu amani, kama vile alivyoahidi, basi, rudini kwenu katika nchi ambayo mlipewa na Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, iwe mali yenu, yaani ngambo ya mto Yordani. Muwe waangalifu kutii amri na sheria ambazo Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliwaamuru: Kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mfuate anachotaka na kushika amri zake; mkae pamoja naye na kumtumikia kwa moyo wote na roho yote.” Basi, Yoshua akawabariki na kuwaruhusu waende zao akawaambia, “Rudini makwenu na utajiri mwingi; ng'ombe wenu wote, fedha, dhahabu, shaba, chuma na mavazi mengi. Gawaneni na ndugu zenu nyara zote mlizoziteka kutoka kwa maadui zenu.” Mose alikuwa ameyapa nusu ya kabila la Manase sehemu yao huko Bashani. Naye Yoshua akaipatia nusu ya pili ya kabila hilo sehemu yao huko magharibi ya mto Yordani kama alivyoyapa makabila yale mengine. *** Basi, watu wa Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase wakaachana na watu wa makabila mengine ya Israeli huko Shilo, nchini Kanaani, wakarudi kwao katika nchi ya Gileadi, nchi yao wenyewe waliyoimiliki kwa amri ya Mwenyezi-Mungu kama alivyomwagiza Mose. Walipofika kwenye mto Yordani wakiwa bado katika nchi ya Kanaani, wakajenga madhabahu kubwa sana karibu na mto huo. Basi, habari zikawafikia watu wa makabila mengine ya Israeli kwamba makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase yalikuwa yamejenga madhabahu kubwa karibu na mto Yordani katika nchi ya Kanaani, yaani ndani ya eneo lao. Waliposikia hivyo, Waisraeli walikusanyika wote huko Shilo kwenda kupigana vita na hayo makabila ya mashariki. Basi, watu wa Israeli wakamtuma Finehasi, mwanawe kuhani Eleazari, huko Gileadi kwa makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase. Finehasi akaondoka pamoja na wakuu kumi, kila mmoja akiwa mkuu wa jamaa katika kabila lake. Nao wakawaendea watu wa makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase huko Gileadi wakawaambia, “Jumuiya nzima ya Mwenyezi-Mungu inauliza hivi: ‘Ni udanganyifu gani huu mmemfanyia Mungu wa Israeli? Mbona mmemwasi Mwenyezi-Mungu kwa kujenga madhabahu hii? Je, dhambi tulizotenda huko Peori hazitoshi? Hamwoni kwamba bado hatujajitakasa na kwamba mateso yake bado yanaisumbua jumuiya ya Mwenyezi-Mungu? Kwa nini, basi, mmeacha kumfuata Mwenyezi-Mungu? Mkimwasi Mwenyezi-Mungu leo, kesho ataikasirikia sana jumuiya nzima ya Israeli. Haya, ikiwa nchi yenu si najisi, njoni katika nchi ya Mwenyezi-Mungu ambako hema yake iko na kujichukulia sehemu huko pamoja nasi; ila tu msimwasi Mwenyezi-Mungu na kutufanya sisi sote waasi kwa kujijengea nyinyi wenyewe madhabahu isiyo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Je, Akani mwana wa Zera alipokosa uaminifu katika vitu vitakatifu, ghadhabu haikuangukia jumuiya nzima ya Israeli? Tena Akani hakufa tu yeye peke yake kwa sababu ya uovu wake.’” Hapo watu wa makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase wakawajibu viongozi wa jamaa za Israeli, “Mungu wa miungu ndiye Mwenyezi-Mungu! Mungu wa miungu ndiye Mwenyezi-Mungu! Yeye anajua kwa nini tumefanya hivyo. Na Waisraeli wote watajua pia! Kama huu ni uasi au ni ukosefu wa imani kwa Mwenyezi-Mungu basi, yeye aache kutuokoa leo. Kama tumemwacha Mwenyezi-Mungu tukajenga madhabahu yetu wenyewe ili tutoe sadaka za kuteketezwa, za nafaka au za amani, basi Mwenyezi-Mungu na atulipize kisasi. Lakini sivyo ilivyo. Tuliijenga kwa kuogopa kwamba huenda katika siku zijazo watoto wenu watawaambia watoto wetu, ‘Nyinyi mna uhusiano gani na Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli? Hamwoni kwamba Mwenyezi-Mungu ameweka mto wa Yordani kuwa mpaka kati yenu na sisi? Nyinyi makabila ya Reubeni na kabila la Gadi hamna fungu lolote lenu kwa Mwenyezi-Mungu.’ Hivyo watoto wenu wangeweza baadaye kusababisha watoto wetu waache kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Ndiyo maana tuliamua kujenga madhabahu hii, lakini si kwa ajili ya kutolea juu yake sadaka wala tambiko, bali tulitaka madhabahu hii iwe ushuhuda kati yetu na nyinyi na vizazi vyetu vijavyo kwamba sisi tunayo haki ya kumtumikia Mwenyezi-Mungu kwa sadaka zetu za kuteketezwa na tambiko zetu, na kwa sadaka zetu za amani, ili watoto wenu wasije wakawaambia watoto wetu kwamba hawana fungu lolote lao kwa Mwenyezi-Mungu. Tena tulifikiri kwamba ikiwa jambo kama hilo litasemwa juu yetu au juu ya wazawa wetu katika siku zijazo, tutasema, ‘Tazameni mfano wa madhabahu ya Mwenyezi-Mungu ambayo wazee wetu waliijenga; sio kwa ajili ya kutolea juu yake sadaka au tambiko bali kama ushuhuda kati yetu na nyinyi’. Sisi hatukuwa na nia ya kumwasi sasa Mwenyezi-Mungu hata kidogo na kumwacha kwa kujenga madhabahu ya kutolea sadaka za kuteketezwa au sadaka za unga au za tambiko. Hatupendi kutolea sadaka mahali pengine isipokuwa juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu iliyo mbele ya maskani yake.” Kuhani Finehasi, viongozi wa jumuiya nzima na wakuu wa jamaa za Israeli waliokuwa pamoja naye waliposikia maneno hayo ya watu wa makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase, wakaridhika. Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akayaambia makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase, “Leo tumejua kwamba Mwenyezi-Mungu yumo miongoni mwenu maana hamkumfanyia Mungu uasi. Sasa mmewaokoa Waisraeli wasiadhibiwe na Mwenyezi-Mungu.” Basi, Finehasi mwana wa kuhani Eleazari pamoja na viongozi wenzake wakawaaga watu wa makabila ya Reubeni na Gadi wakaondoka nchini Gileadi, wakarudi Kanaani kwa Waisraeli na kuwapa habari hizo. Taarifa hiyo ikawafurahisha Waisraeli, wakamshukuru Mwenyezi-Mungu na kuacha mipango yao ya vita na lengo lao la kuharibu kabisa nchi iliyokuwa ya makabila ya Reubeni na Gadi. Watu wa makabila ya Reubeni na Gadi wakaiita ile madhabahu ya “Ushuhuda,” kwani walisema, “Madhababu hii ni ushahidi wetu kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu.” Baada ya muda mrefu, Mwenyezi-Mungu aliwajalia Waisraeli amani kwa kuwaokoa na maadui zao pande zote. Wakati huo Yoshua alikuwa mzee wa miaka mingi. Yoshua aliwaita Waisraeli wote pamoja na viongozi na wazee wao, waamuzi na maofisa, akawaambia, “Sasa mimi nimekuwa mzee wa miaka mingi. Nyinyi mmeona mambo yote Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliyoyatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Mwenyezi-Mungu Mungu wenu ndiye aliyewapigania. Nchi za mataifa yaliyobaki na yale niliyoyaangamiza nimewagawieni ziwe mali ya makabila yenu, kutoka Yordani mpaka bahari ya Mediteranea, upande wa magharibi. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawaondoa mbele yenu na kuwafukuza kabisa, nanyi mtaimiliki nchi yao kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaahidi. Kwa hiyo, muwe imara katika kuzingatia yote yaliyoandikwa katika kitabu cha sheria ya Mose, kamwe msiyaache. Msishirikiane na mataifa haya yaliyobaki kati yenu. Msiitaje miungu yao wala msiape kwa majina ya miungu yao; msiitumikie wala msiisujudie. Bali ambataneni na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kama mlivyofanya mpaka leo. Maana Mwenyezi-Mungu ameyafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu na hakuna mtu ambaye ameweza kuwapinga nyinyi hadi leo. Mtu wenu mmoja tu anaweza kuwakimbiza maadui elfu, kwani Mwenyezi-Mungu Mungu wenu ndiye anayewapigania kama alivyowaahidi. Basi, muwe waangalifu sana kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Maana, kama mkimwasi Mwenyezi-Mungu na kujiunga na mataifa haya yaliyobaki kati yenu, mkaoa kwao nao wakaoa kwenu, jueni kwa hakika kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, hataendelea kuyafukuza mataifa haya mbele yenu, bali yatakuwa kwenu kikwazo na mtego. Yatakuwa kwenu mjeledi wa kuwachapeni na miiba ya kuwachomeni machoni mpaka hapo mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni. “Sasa, wakati wangu wa kufariki dunia kama ilivyo kawaida ya walimwengu wote umekaribia. Lakini nyinyi nyote mnajua wazi mioyoni na rohoni mwenu kwamba katika mambo yote mema ambayo Mwenyezi-Mungu Mungu wenu aliwaahidi, hakuna hata moja ambalo halikutimia. Yote yametimia kama vile alivyoahidi. Lakini kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyotimiza mambo yote mema aliyowaahidi, vivyo hivyo anaweza kuwaletea maovu yote mpaka awaangamize nyote kutoka nchi hii nzuri ambayo amewapeni. Kama mkivunja agano lake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambalo aliwaamuru mlishike, mkaenda kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu itawaka juu yenu, nanyi mtaangamia mara moja kutoka nchi hii nzuri ambayo amewapeni.” Kisha Yoshua akayakusanya makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maofisa wa Israeli, nao wakaja mbele ya Mungu. Yoshua akawaambia watu wote, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: Hapo zamani, wazee wenu waliishi ngambo ya mto Eufrate, wakaitumikia miungu mingine. Mzee mmoja alikuwa Tera, baba yao Abrahamu na Nahori. Mimi Mungu nilimwondoa babu yenu Abrahamu kutoka huko ngambo ya mto Eufrate na kumleta hapa Kanaani, ambako nilimpatia wazawa wengi. Nilimpa Isaka, naye Isaka nikampa Yakobo na Esau. Nilimpa Esau milima ya Seiri aimiliki. Lakini Yakobo na watoto wake walikwenda Misri. Baadaye niliwatuma Mose na Aroni, nikailetea nchi ya Misri mapigo, na baadaye nikawatoa nyinyi nchini humo. Niliwatoa wazee wenu kutoka Misri na kuwaleta hadi kwenye bahari ya Shamu. Wamisri waliwafuatia wakiwa na magari na askari wapandafarasi. Waisraeli waliponililia mimi Mwenyezi-Mungu, niliweka giza kati yao na Wamisri na kuifanya bahari iwafunike Wamisri. Nyinyi wenyewe mlijionea yale niliyowatendea Wamisri. Mliishi jangwani muda mrefu. Kisha niliwaongoza hadi katika nchi ya Waamori ambao waliishi upande mwingine wa mto Yordani. Walipigana nanyi, lakini mimi niliwapeni ushindi juu yao mkawaangamiza na kuiteka nchi yao. Naye Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, akaja na kuwashambulia Waisraeli. Akamwalika Balaamu mwana wa Beori aje kuwalaani nyinyi. Lakini mimi sikumsikiliza Balaamu, naye ikambidi kuwabariki, nami nikawaokoa nyinyi mikononi mwa Balaki. Halafu mkavuka mto Yordani, mkafika Yeriko. Wakazi wa Yeriko walipigana nanyi, hali kadhalika na Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi. Hao mimi nikawatia mikononi mwenu. Nilituma manyigu mbele yenu ambayo yaliwatimua wafalme wawili wa Waamori. Hamkufanya haya kwa kupania mapanga wala pinde zenu. “Niliwapeni mashamba ambayo hamkuwa mmeyalima, na miji ambayo hamkuijenga ambamo sasa mnaishi, na kula matunda ya mizabibu na mizeituni ambayo hamkuipanda. “Sasa, basi, mcheni Mwenyezi-Mungu na kumtumikia kwa moyo mnyofu na uaminifu. Acheni kabisa miungu ile ambayo wazee wenu waliiabudu ngambo ya mto Eufrate na nchini Misri. Mtumikieni Mwenyezi-Mungu. Kama hamtaki kumtumikia Mwenyezi-Mungu, basi chagueni leo hii ni nani mtakayemtumikia: Kwamba ni miungu ile ambayo wazee wenu waliitumikia ngambo ya mto Eufrate, au miungu ya Waamori ambao sasa mnaishi nchini mwao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Mwenyezi-Mungu.” Hapo watu wakamjibu, “Hatutaweza kamwe kumwacha Mwenyezi-Mungu na kuitumikia miungu mingine. Maana, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ndiye aliyetutoa sisi pamoja na wazee wetu katika nchi ya Misri tulikokuwa watumwa, tukayaona kwa macho yetu wenyewe matendo ya ajabu aliyotenda. Akatulinda katika safari zetu zote na miongoni mwa watu wote ambao tulipita kati yao. “Mwenyezi-Mungu alituondolea watu wote yaani Waamori wote waliokaa nchini. Kwa hiyo, nasi tutamtumikia Mwenyezi-Mungu, maana ndiye Mungu wetu.” Lakini Yoshua akawaambia, “Nyinyi hamwezi kumtumikia Mwenyezi-Mungu, maana yeye ni Mungu Mtakatifu. Yeye ni Mungu mwenye wivu, naye hatawasamehe makosa na dhambi zenu. Mkimwacha Mwenyezi-Mungu na kuitumikia miungu ya kigeni, atawaadhibu na kuwaangamiza kabisa, hata ingawa amewatendea mema haya yote.” Nao watu wakamwambia Yoshua, “La, hasha! Sisi tutamtumikia Mwenyezi-Mungu tu.” Hapo Yoshua akawaambia, “Nyinyi wenyewe ni mashahidi wa nafsi zenu kwamba mmechagua kumtumikia Mwenyezi-Mungu.” Nao wakamjibu, “Sisi tu mashahidi.” Naye akawaambia, “Basi, ondoeni miungu ya kigeni mliyo nayo, mkamfuate Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wenu wote.” Nao, wakasema, “Tutamtumikia na kumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.” Hivyo, Yoshua akafanya agano na Waisraeli huko Shekemu, akawapa masharti na maagizo ya kufuata. Yoshua akayaandika haya yote katika kitabu cha sheria ya Mungu; kisha, akachukua jiwe kubwa na kulisimika chini ya mwaloni katika hema ya Mwenyezi-Mungu. Halafu akawaambia watu wote, “Jiwe hili ndilo litakalokuwa shahidi kwetu, maana limesikia maneno yote ambayo Mwenyezi-Mungu ametuambia. Kwa hiyo, litashuhudia dhidi yenu, ili msije mkamkana Mungu wenu.” Halafu Yoshua akawaruhusu watu waondoke; nao wakaenda kila mmoja kwake. Baada ya mambo hayo, Yoshua, mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, akafariki akiwa na umri wa miaka 110. Nao wakamzika kwenye eneo ambalo alikuwa amegawiwa kuwa sehemu yake, huko Timnath-sera, katika milima ya Efraimu, kaskazini ya mlima wa Gaashi. Waisraeli walimtumikia Mwenyezi-Mungu muda wote wa uhai wa Yoshua, na baada ya kifo chake, waliendelea kumtumikia kwa muda walioishi wale wazee waliokuwa wameona kwa macho yao mambo yale Mwenyezi-Mungu aliyowatendea Waisraeli. Mifupa ya Yosefu ambayo Waisraeli walikuwa wameileta kutoka Misri waliizika huko Shekemu katika eneo ambalo Yakobo alikuwa amelinunua kutoka kwa wana wa Hamori, baba yake Shekemu, kwa vipande 100 vya fedha. Ardhi hii nayo ikawa mali yao wazawa wa Yosefu. Naye Eleazari, mwana wa Aroni, akafariki na kuzikwa Gibea, mji ambao alikuwa amepewa mwanawe Finehasi katika nchi ya milima ya Efraimu. Baada ya kifo cha Yoshua, Waisraeli walimwuliza Mwenyezi-Mungu: “Mwenyezi-Mungu, ni kabila gani litakwenda kupigana kwanza na Wakanaani?” Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Kabila la Yuda litakwenda kupigana nao kwanza, maana nimeitia nchi hiyo mikononi mwao.” Watu wa kabila la Yuda wakawaambia ndugu zao, watu wa kabila la Simeoni, “Shirikianeni nasi tunapokwenda kuitwaa nchi hiyo ambayo tumepewa. Nasi, pia tutashirikiana nanyi kwenda kuitwaa nchi mtakayopewa.” Hivyo kabila la Simeoni likakubali kushirikiana nao. Basi, watu wa kabila la Yuda wakaenda kufanya mashambulio, naye Mwenyezi-Mungu akawatia Wakanaani na Waperizi mikononi mwao, wakawaua watu 10,000 katika vita huko Bezeki. Katika mji huo walimkuta mfalme Adoni-bezeki, wakapigana naye na kuwashinda Wakanaani na Waperizi. Adoni-bezeki akakimbia, lakini walimfuatia, wakamkamata, wakamkata vidole gumba vya mikono na miguu. Adoni-bezeki akasema, “Wafalme sabini waliokatwa vidole gumba vya mikono na miguu waliokota makombo chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa kama nilivyotenda.” Wakampeleka Yerusalemu, akafia huko. Watu wa kabila la Yuda waliushambulia mji wa Yerusalemu na kuuteka. Waliwaua wakazi wake kwa mapanga na kuuteketeza mji kwa moto. Baadaye, watu wa kabila la Yuda walikwenda kupigana na Wakanaani walioishi kwenye nchi ya milima, Negebu na kwenye nchi tambarare. Waliwashambulia pia Wakanaani walioishi katika mji wa Hebroni ambao hapo awali uliitwa Kiriath-arba, wakashinda makabila ya Sheshai, Himani na Talmai. Kutoka huko watu wa kabila la Yuda walikwenda kuushambulia mji wa Debiri; ambao hapo awali uliitwa Kiriath-seferi. Kalebu akatangaza: “Mtu yeyote atakayefaulu kuuteka mji wa Kiriath-seferi, nitamwoza binti yangu Aksa.” Basi, Othnieli, mwana wa Kenazi na mdogo wake Kalebu, akauteka, naye Kalebu akamtoa bintiye Aksa aolewe na Othnieli. Aksa alipowasili kwa Othnieli, akamwambia Othnieli amwombe Kalebu baba yake shamba. Aksa alikuwa amepanda punda na aliposhuka chini baba yake alimwuliza, “Ungependa nikupe nini?” Akamjibu, “Nipe zawadi! Naomba unipe chemchemi za maji kwani eneo ulilonipa huko Negebu ni kavu.” Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini. Wazawa wa Keni ambaye alikuwa baba mkwe wa Mose, walifuatana na watu wa kabila la Yuda kutoka Mji wa Mitende yaani mji wa Yeriko, mpaka jangwa la Yuda karibu na Aradi, wakafanya makao yao huko pamoja na watu wa Yuda. Watu wa kabila la Yuda walishirikiana na ndugu zao, watu wa kabila la Simeoni, wakawashinda Wakanaani waliokaa Sefathi. Waliuangamiza kabisa mji huo na kugeuza jina lake kuwa Horma. Watu wa kabila la Yuda pia waliteka miji ya Gaza na eneo lake, Ashkeloni na eneo lake, na Ekroni na eneo lake. Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na watu wa kabila la Yuda, nao wakaiteka nchi ya milima. Lakini hawakuweza kuwashinda wenyeji wa nchi tambarare kwa sababu magari yao ya vita yalikuwa ya chuma. Mji wa Hebroni ukakabidhiwa kwa Kalebu kufuatana na maagizo ya Mose. Kalebu akazifukuza kutoka huko koo tatu za Anaki. Lakini watu wa kabila la Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa mjini Yerusalemu; ndiyo maana Wayebusi wanakaa pamoja na watu wa kabila la Benyamini mjini Yerusalemu mpaka leo. Watu wa makabila ya Yosefu waliushambulia mji wa Betheli, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja nao. Kwanza walikuwa wamewatuma wapelelezi kwenda kuupeleleza mji wa Betheli. Mji huo hapo awali uliitwa Luzu. Wapelelezi hao walimwona mtu mmoja akitoka mjini, wakamwambia, “Tafadhali, tuoneshe njia inayoingia mjini, nasi tutakutendea kwa wema.” Akawaonesha njia ya kuingia mjini. Basi, wakaingia na kuangamiza kila mtu aliyekuwamo. Lakini wakamwacha salama mtu huyo na jamaa yake. Mtu huyo akahamia nchi ya Wahiti, huko akajenga mji ambao aliuita Luzu; na mji huo unaitwa hivyo mpaka leo. Watu wa kabila la Manase hawakuwafukuza wakazi wa miji ya Beth-sheani na vijiji vyake, Taanaki na vijiji vyake, Dori na vijiji vyake, Ibleamu na vijiji vyake, na Megido pamoja na vijiji vyake. Wakanaani waliendelea kukaa huko. Hata Waisraeli walipokuwa na nguvu hawakuwafukuza Wakanaani bali waliwapa kazi za kulazimishwa. Watu wa kabila la Efraimu hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Gezeri, na hawa waliishi huko pamoja na watu wa Efraimu. Watu wa kabila la Zebuluni hawakuwafukuza wakazi wa mji wa Kitroni, wala wale wa mji wa Nahalali, waliendelea kukaa pamoja nao wakiwafanyiza kazi za kulazimishwa. Watu wa kabila la Asheri hawakuwafukuza wakazi wa miji ya Ako, Sidoni, Alabu, Akzibu, Helba, Afeka na Rehobu. Watu wa kabila la Asheri walikaa pamoja na Wakanaani wenyeji wa nchi hiyo kwani hawakuwafukuza. Watu wa kabila la Naftali hawakuwafukuza wakazi wa mji wa Beth-shemeshi au wakazi wa Beth-anathi, lakini walikaa pamoja nao. Hata hivyo wenyeji wa miji hiyo, walilazimishwa kuwafanyia Waisraeli kazi za kulazimishwa. Waamori waliwafukuzia watu wa kabila la Dani milimani. Hawakuwaruhusu kuja kuishi katika nchi tambarare. Waamori waliendelea kuishi katika miji iliyokuwa katika kilima cha Heresi, Aiyaloni na Shaalbimu. Lakini watu wa makabila ya Manase na Efraimu waliwatawala Waamori na kuwafanya wafanye kazi za kulazimishwa. Mpaka wa Waamori ulikuwa kaskazini ya Sela, kupitia pitio la Akarimu. Malaika wa Mwenyezi-Mungu aliondoka Gilgali, akaenda Bokimu, akawaambia Waisraeli, “Niliwatoa nchini Misri na kuwaleta katika nchi ambayo niliwaahidi kwa kiapo babu zenu. Nilisema kwamba sitalivunja agano langu nanyi kamwe. Na kwa upande wenu niliwaamuru msifanye agano na wenyeji wa nchi hii na kwamba madhabahu zao mtazibomoa. Lakini nyinyi hamkuitii amri yangu. Kwa nini mambo haya? Kwa hiyo sasa nasema: Sitawafukuza tena wakazi wa nchi hii bali watawataabisha, nayo miungu yao itakuwa mtego kwenu.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu alipowaambia watu wote wa Israeli maneno haya, walipaza sauti zao na kulia. Wakapaita mahali hapo Bokimu. Hapo wakamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu. Baada ya Yoshua kuwaaga Waisraeli, kila mmoja alikwenda kwenye eneo lake alilogawiwa ili kuimiliki nchi. Waisraeli walimtumikia Mwenyezi-Mungu siku zote za maisha ya Yoshua na baada ya kifo chake muda wote walioishi wale wazee waliosalia ambao waliyaona matendo makuu ambayo Mwenyezi-Mungu aliwatendea Waisraeli. Yoshua mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alifariki akiwa na umri wa miaka 110. Wakamzika katika sehemu aliyogawiwa iwe yake huko Timnath-heresi, katika nchi ya milima ya Efraimu kaskazini ya mlima Gaashi. Kisha watu wote wa kizazi chake walifariki, kikafuata kizazi kingine ambacho hakikumjua Mwenyezi-Mungu wala matendo aliyowatendea watu wa Israeli. Basi, Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu Mabaali. Walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao, ambaye aliwatoa katika nchi ya Misri, wakaifuata miungu mingine, miungu iliyoabudiwa na watu walioishi kandokando yao. Waliisujudia miungu hiyo, wakamkasirisha sana Mwenyezi-Mungu. Walimwacha Mwenyezi-Mungu, wakatumikia Mabaali na Maashtarothi. Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya Israeli, naye akawaacha wanyanganyi wapore mali zao. Aliwakabidhi kwa adui zao waliowazunguka hata wasiweze tena kuwapinga. Kila walipokwenda kupigana, mkono wa Mwenyezi-Mungu uliwakabili kuwaletea balaa, kama alivyokuwa amewaonya na kuapa. Nao wakawa katika huzuni kubwa. Ndipo Mwenyezi-Mungu akawapa waamuzi ambao waliwaokoa mikononi mwa watu waliopora mali zao. Hata hivyo, Waisraeli hawakuwasikiliza waamuzi wao, maana walifanya kama wazinzi kwa kufuata miungu mingine na kuisujudia. Waliacha upesi nyayo walizofuata babu zao ambao walitii amri za Mwenyezi-Mungu; bali wao hawakufanya hivyo. Kila mara Mwenyezi-Mungu alipowapelekea mwamuzi, yeye mwenyewe alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa mikononi mwa adui zao muda wote wa uhai wa mwamuzi huyo. Aghalabu, Mwenyezi-Mungu aliwaonea huruma aliposikia kilio chao kutokana na mateso na dhuluma walizofanyiwa. Lakini kila mara mwamuzi alipofariki walirudia mienendo yao ya zamani, wakaishi vibaya kuliko babu zao. Waliifuata miungu mingine, wakaitumikia na kuisujudia, wala hawakuyaacha matendo yao wala ukaidi wao. Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akawaka hasira dhidi ya Waisraeli, akasema, “Kwa kuwa watu hawa wamevunja agano nililofanya na babu zao, wakakataa kutii sauti yangu, sitayafukuza tena mataifa ambayo Yoshua aliyabakiza, wakati alipofariki. Nitayatumia mataifa hayo kuwajaribu Waisraeli nione kama watairudia njia yangu kama babu zao au sivyo.” Basi, Mwenyezi-Mungu akayaacha mataifa hayo, wala hakuyafukuza mara moja, wala hakumpa Yoshua ushindi juu ya mataifa hayo! Mwenyezi-Mungu aliyaacha nchini mataifa yafuatayo ili kuwajaribu Waisraeli ambao walikuwa hawajapigana vita katika nchi ya Kanaani (alifanya hivyo ili awape watu wa vizazi hivyo ujuzi wa kupigana kwani hawakuwa wameona vita): Wakuu watano wa Wafilisti, Wakanaani wote, Wasidoni na Wahivi waliohamia katika milima ya Lebanoni kutoka mlima Baal-hermoni mpaka kufikia Hamathi. Mwenyezi-Mungu alikusudia kuwatumia hao ili awajaribu Waisraeli, aone kama watatii amri zake alizowaamuru wazee wao kwa njia ya Mose. Basi, Waisraeli waliishi pamoja na Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Wakaoa binti zao na kuoza binti zao kwa vijana wa mataifa hayo na kuiabudu miungu yao. Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; wakamsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakaabudu Mabaali na Maashera. Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia, nao wakamtumikia kwa muda wa miaka minane. Waisraeli wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawapelekea mtu wa kuwakomboa yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu. Basi, roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Othnieli, naye akawa mwamuzi wa Waisraeli. Othnieli alikwenda vitani naye Mwenyezi-Mungu akamtia Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia mikononi mwake. Hivyo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini. Kisha Othnieli mwana wa Kenazi, akafariki. Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akampa nguvu mfalme Egloni wa Moabu awashambulie Waisraeli, kwa sababu walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Egloni akawakusanya Waamoni na Waamaleki, akaenda kupigana na Waisraeli, akawashinda. Akauteka Mji wa Mitende yaani Yeriko. Waisraeli wakamtumikia Egloni mfalme wa Moabu, kwa muda wa miaka kumi na minane. Lakini Waisraeli walipomlilia Mwenyezi-Mungu, yeye aliwapelekea mtu wa kuwakomboa, yaani Ehudi mwana wa Gera, mwenye mkono wa shoto, wa kabila la Benyamini. Waisraeli walimtuma apeleke zawadi zao kwa Egloni mfalme wa Moabu. Ehudi akajitengenezea upanga wenye makali kuwili; urefu wake sentimita hamsini. Akaufunga kiunoni mwake upande wa kulia ndani ya mavazi yake. Kisha akampelekea Egloni zile zawadi. Egloni alikuwa mtu mnene sana. Ehudi alipomaliza kutoa zawadi, akawaambia watu waliobeba zawadi, waondoke. Lakini yeye alipofika kwenye sanamu za mawe yaliyochongwa karibu na Gilgali, alimrudia Egloni akasema, “Nina ujumbe wa siri kwako, ee mfalme.” Mfalme akawaamuru watumishi wakae kimya, nao wakatoka nje. Naye Ehudi akamkaribia pale alipokaa katika chumba chake chenye baridi barazani, akamwambia “Nina ujumbe wako kutoka kwa Mungu.” Mfalme akainuka kitini mwake na kusimama. Ehudi akauchomoa upanga wake kwa mkono wake wa kushoto kutoka paja lake la kulia, akamchoma nao tumboni mwake. Upanga ukaingia ndani pamoja na mpini wake, mafuta yakaufunika upanga huo kwani Ehudi hakuutoa tena; ukawa umetokea kwa nyuma. Kisha, Ehudi akatoka nje barazani baada ya kuifunga milango ya chumba hicho kwa ufunguo. Ehudi alipoondoka, watumishi wa mfalme wakarudi. Walipoona milango yote ya chumba imefungwa, walifikiri amekwenda kujisaidia chooni humo ndani ya nyumba. Wakangojea mpaka wakaanza kuwa na wasiwasi. Walipoona hafungui, wakachukua ufunguo na kufungua mlango. Wakamwona mfalme wao sakafuni, naye amekufa. Walipokuwa wanangoja, Ehudi alitoroka akipitia kwenye sanamu za mawe, akaenda Seira. Alipofika huko alipiga tarumbeta katika nchi ya milima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka huko milimani naye akawatangulia. Akawaambia, “Mnifuate, maana Mwenyezi-Mungu amewatia adui zenu Wamoabu mikononi mwenu.” Wakamfuata mpaka kivuko cha Yordani na kukiteka toka mikononi mwa Wamoabu, wakazuia mtu yeyote kupita. Siku hiyo, wakawaua Wamoabu wapatao 10,000; watu wote wenye afya na nguvu, wala hakuna hata mmoja aliyenusurika. Siku hiyo Waisraeli wakawashinda Wamoabu. Nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka themanini. Baada ya Ehudi mwana wa Anati, Shamgari alishika nafasi yake. Yeye aliwaua Wafilisti 600 kwa fimbo ya kuchungia ng'ombe. Naye pia aliwakomboa Waisraeli. Baada ya kifo cha Ehudi, Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, ambaye aliishi huko Hazori. Kamanda wa jeshi lake alikuwa Sisera, mwenyeji wa Harosheth-hagoimu. Mfalme Yabini alikuwa na magari ya vita 900 ya chuma. Aliwakandamiza sana Waisraeli kwa miaka ishirini; nao wakamlilia Mwenyezi-Mungu awasaidie. Wakati huo, kulikuwa na nabii mwanamke aliyeitwa Debora, mke wa Lapidothi, aliyekuwa mwamuzi wa Waisraeli wakati huo. Debora alikuwa na mazoea ya kuketi chini ya mtende uliokuwa kati ya mji wa Rama na mji wa Betheli katika nchi ya milima ya Efraimu. Watu wa Israeli walimjia ili awaamulie mashauri yao. Siku moja alimwita Baraki mwana wa Abinoamu wa Kedeshi katika nchi ya Naftali. Alipokuja alimwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anakuamuru hivi: ‘Nenda ukusanye watu wako mlimani Tabori, uchague watu 10,000 kutoka makabila ya Naftali na Zebuluni. Mimi nitamchochea Sisera, jemadari wa jeshi la Yabini, aje na majeshi na magari yake kupigana nawe kwenye mto Kishoni, na kumtia mikononi mwako.’” Baraki akamwambia Debora, “Kama utakwenda pamoja nami, nitakwenda. Lakini usipokwenda pamoja nami, sitakwenda.” Debora akamjibu, “Sawa. Nitakwenda pamoja nawe; lakini hutapata heshima yoyote ya ushindi, maana Mwenyezi-Mungu, atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Basi, Debora akafuatana na Baraki kwenda Kedeshi. Baraki akayaita makabila ya Naftali na Zebuluni huko Kedeshi; watu 10,000 wakamfuata. Debora akaenda pamoja naye. Wakati huo, Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wenzake ambao ni wazawa wa Hobabu, baba mkwe wa Mose. Alikuwa amepiga hema lake mbali huko kwenye mwaloni wa Zaananimu, karibu na Kedeshi. Sisera alipopata habari kwamba Baraki mwana wa Abinoamu amekwenda mlimani Tabori, alikusanya jeshi lake lote na magari yake mia tisa ya chuma, akaondoka Harosheth-hagoimu, akaenda kwenye mto Kishoni. Debora akamwambia Baraki, “Inuka! Leo ni siku ambayo Mwenyezi-Mungu atamtia Sisera mikononi mwako. Mwenyezi-Mungu anakwenda mbele yako.” Basi, Baraki akashuka kutoka mlimani Tabori akiwaongoza watu wake 10,000. Baraki akafanya mashambulizi, naye Mwenyezi-Mungu akamtimua Sisera na jeshi lake lote mbele ya Baraki kwa upanga. Sisera akatoka katika gari lake, akakimbia kwa miguu. Baraki akalifuatia jeshi hilo na magari mpaka Harosheth-hagoimu na kuwaua wanajeshi wote wa Sisera kwa mapanga; hakubaki hata mtu mmoja. Lakini Sisera alikimbia kwa miguu mpaka hemani kwa Yaeli, mke wa Heberi, Mkeni. Alifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na amani kati ya mfalme Yabini wa Hazori na jamaa ya Heberi. Yaeli akatoka kumlaki Sisera, akamwambia, “Bwana wangu, karibu kwangu, wala usiogope.” Akaingia hemani mwake, akamfunika kwa blanketi. Sisera akamwambia Yaeli, “Tafadhali, nipe maji kidogo ninywe, maana nina kiu.” Akampa maziwa badala ya maji, kisha akamfunika tena. Sisera akamwambia, “Simama mlangoni mwa hema. Mtu yeyote akija kukuuliza kama kuna mtu yeyote hapa, mwambie hakuna.” Lakini Yaeli, mke wa Heberi, akachukua kigingi cha hema na nyundo, akamwendea polepole akakipigilia kile kigingi cha hema katika paji la uso wake kikapenya mpaka udongoni, kwa maana alikuwa amelala fofofo kwa uchovu. Basi, Sisera akafa papo hapo. Naye Baraki alipokuwa anamfuatilia Sisera, Yaeli akatoka nje kumlaki akamwambia, “Njoo nami nitakuonesha yule unayemtafuta.” Baraki akaingia ndani ya hema la Yaeli na kumkuta Sisera chini, amekufa, na kigingi cha hema pajini mwake. Hivyo, siku hiyo Mungu akawapa Waisraeli ushindi juu ya mfalme Yabini wa Kanaani. Waisraeli wakaendelea kumwandama Yabini, mfalme wa Kanaani, mpaka walipomwangamiza. Siku hiyo, Debora na Baraki, mwana wa Abinoamu, wakaimba wimbo huu: “Viongozi walijitokeza kuongoza Israeli, watu walijitolea kwa hiari yao. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu! “Sikilizeni, enyi wafalme! Tegeni sikio, enyi wakuu! Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. “Ee Mwenyezi-Mungu, ulipotoka huko Seiri, ulipoteremka mlimani Edomu, nchi ilitetemeka, mbingu zilidondosha maji, naam, mawingu yakaiangusha mvua. Milima ilitikisika mbele yako Mwenyezi-Mungu, naam, mlima Sinai mbele yako Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. “Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi, katika wakati wa Yaeli, misafara ilikoma kupita nchini, wasafiri walipitia vichochoroni. Wakulima walikoma kuwako, walikoma kuwako katika Israeli, mpaka nilipotokea mimi Debora, mimi niliye kama mama wa Israeli. Walijichagulia miungu mipya, kukawa na vita katika nchi. Lakini hakukupatikana mwenye upanga au ngao kati ya watu 40,000 wa Israeli. Nawapa heshima makamanda wa Israeli waliojitoa kwa hiari yao kati ya watu. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu! “Tangazeni, enyi wapandapunda weupe, enyi mnaokalia mazulia ya fahari, nyinyi mnaotembea njiani, tangazeni jambo hilo. Imbeni kupita wanamuziki kwenye visima vya maji, tangazeni ushindi wa Mwenyezi-Mungu, ushindi kwa wakulima wake katika Israeli. Ndipo watu wa Mwenyezi-Mungu waliposhuka malangoni. “Amka, amka, Debora! Amka! Amka uimbe wimbo! Amka, Baraki mwana wa Abinoamu, uwachukue mateka wako. Mashujaa waliobaki waliteremka, watu wa Mwenyezi-Mungu walikwenda kumpigania dhidi ya wenye nguvu. Kutoka Efraimu waliteremka bondeni, wakafuata ndugu zao watu wa Benyamini; kutoka Makiri walishuka makamanda, kutoka Zebuluni maofisa wakuu. Wakuu wa Isakari wakafuatana na Debora, watu wa Isakari waaminifu kwa Baraki; wakamfuata mbio mpaka bondeni. Lakini miongoni mwa koo za Reubeni kulikuwamo kusitasita kwingi. Kwa nini walibaki mazizini? Ili kusikiliza milio ya kondoo? Miongoni mwa koo za Reubeni kulikuwamo kusitasita kwingi. Kabila la Gileadi lilibaki ngambo ya Yordani. Kabila la Dani, kwa nini mlibaki merikebuni? Kabila la Asheri lilitulia huko pwani ya bahari, lilikaa bandarini mwake. Watu wa Zebuluni ni watu waliohatarisha maisha yao katika kifo. Hata wa Naftali walikikabili kifo kwenye miinuko ya mashamba. “Huko Taanaki, kando ya chemchemi za Megido, wafalme walikuja, wakapigana; wafalme wa Kanaani walipigana, lakini hawakupata nyara za fedha. Nyota kutoka mbinguni zilishiriki vita, zilifuata njia zao, zilipigana na Sisera. Mafuriko ya mto Kishoni yaliwachukua mbali, naam, mafuriko makali ya mto Kishoni. Songa mbele kwa nguvu, ee nafsi yangu! “Farasi walipita wakipiga shoti;, walikwenda shoti na kishindo cha kwato zao. Malaika wa Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Uapizeni mji wa Merosi, waapizeni vikali wakazi wake; maana hawakuja kumsaidia Mwenyezi-Mungu hawakumsaidia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wenye nguvu’. “Abarikiwe kuliko wanawake wote Yaeli, mke wa Heberi, Mkeni. Naam, amebarikiwa kuliko wanawake wote wanaokaa mahemani. Sisera alimwomba maji, naye akampa maziwa; alimletea siagi katika bakuli ya heshima. Kwa mkono mmoja alishika kigingi cha hema, na kwa mkono wake wa kulia nyundo ya fundi; alimponda Sisera kichwa, alivunja na kupasuapasua paji lake. Sisera aliinama, akaanguka; alilala kimya miguuni pake. Hapo alipoinama ndipo alipoanguka, amekufa! “Mama yake Sisera alitazama dirishani alichungulia katika viunzi vyake, akalalamika: ‘Kwa nini gari lake limechelewa? Mbona vishindo vya magari yake vimechelewa kusikika?’ Jibu akalipata kwa wanawake wenye hekima: Akajituliza tena na tena kwa jibu hilo: ‘Bila shaka wanatafuta na kugawana nyara; msichana mmoja au wawili kwa kila askari, vazi la sufu ya rangi kwa ajili ya Sisera. Vazi la sufu iliyotariziwa, na mikufu miwili ya nakshi kwa ajili ya shingo yangu!’ “Ee Mwenyezi-Mungu, waangamie adui zako wote! Lakini rafiki zako na wawe kama jua, wakati linapochomoza kwa mwanga mkubwa!” Nayo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini. Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; naye akawatia mikononi mwa Wamidiani kwa muda wa miaka saba. Wamidiani waliwakandamiza sana Waisraeli, mpaka wakajichimbia mashimo na mapango milimani kuwa ngome zao. Kila mara Waisraeli walipopanda mbegu mashambani, Wamidiani, Waamaleki na watu wengine wa huko mashariki walikuja kuwashambulia. Mataifa hayo yaliweka kambi nchini, yakawashambulia na kuharibu mazao yote nchini hadi mpakani mwa Gaza, wasiwaachie Waisraeli chochote, awe kondoo, ng'ombe au punda. Adui waliozoea kuja kwa wingi kama nzige, pamoja na ng'ombe na ngamia wao na kufanya makao yao nchini Israeli, waliharibu nchi ya Israeli kwa vile walikuwa wengi mno wasiohesabika. Waisraeli walidhoofishwa sana na Wamidiani hata wakamlilia Mwenyezi-Mungu awasaidie. Waisraeli walipomlilia Mwenyezi-Mungu awaondolee taabu walizopata kwa Wamidiani, Mwenyezi-Mungu aliwapelekea nabii, naye akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Niliwatoa nchini Misri ambako mlikuwa watumwa, nikawakomboa mikononi mwa Wamisri wote waliowakandamiza. Nikawafukuza watu mbele yenu na kuwapa nyinyi nchi yao. Kisha nikawakumbusheni kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; na kwamba msiiheshimu miungu ya Waamori, ambao nchi yao mmeichukua, lakini hamkuisikiliza sauti yangu.’” Malaika wa Mwenyezi-Mungu akaenda, akaketi chini ya mwaloni wa Yoashi, Mwabiezeri, huko Ofra. Gideoni mwana wa Yoashi, alikuwa anapura ngano ndani ya shinikizo la kusindikia zabibu ili Wamidiani wasimwone. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nawe, ewe shujaa.” Gideoni akamwambia, “Ee Bwana wangu, ikiwa Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu ambayo wazee wetu walitusimulia, wakisema: ‘Mwenyezi-Mungu ndiye aliyetutoa nchini Misri.’ Lakini sasa Mwenyezi-Mungu ametutupa na kututia mikononi mwa Wamidiani!” Mwenyezi-Mungu akamgeukia, akamwambia, “Nenda kwa uwezo ulio nao, ukaikomboe Israeli kutoka Wamidiani. Ni mimi ninayekutuma.” Gideoni akamjibu, “Tafadhali Bwana, nitawezaje kuikomboa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu zaidi katika kabila la Manase, na mimi mwenyewe ni mdogo kabisa katika jamaa yetu!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nitakuwa pamoja nawe; nawe utawaangamiza Wamidiani kana kwamba wangekuwa mtu mmoja.” Gideoni akamwambia, “Basi, ikiwa nimepata fadhili kwako, nioneshe ishara ili nijue kuwa ni wewe kweli uliyezungumza nami. Nakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea zawadi yangu na kuiweka mbele yako.” Naye akamjibu, “Nitakaa hapa mpaka utakaporudi.” Gideoni akaenda nyumbani mwake, akatayarisha mwanambuzi na mikate isiyotiwa chachu kutoka debe la unga; akatia nyama ndani ya kikapu na mchuzi ndani ya chungu, kisha akampelekea chini ya mwaloni, akampa. Malaika wa Mungu akamwambia, “Chukua nyama na mikate isiyotiwa chachu uviweke juu ya mwamba huu. Halafu tia mchuzi juu ya mikate na nyama.” Naye akafanya hivyo. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akanyosha fimbo yake, akagusa nyama na mikate kwa ncha ya fimbo. Ghafla, moto ukatoka mwambani, ukateketeza nyama na mikate. Mara malaika wa Mwenyezi-Mungu akatoweka mbele yake. Ndipo Gideoni akatambua kwamba huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu; akasema, “Ole wangu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu, maana nimemwona malaika wako uso kwa uso.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Amani iwe nawe! Usiogope, hutakufa.” Gideoni akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu huko na kuyaita, “Mwenyezi-Mungu ni Amani.” Madhabahu hiyo iko huko Ofra, mji wa Wabiezeri, mpaka leo. Usiku huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Chukua fahali mmoja wa baba yako, fahali yule wa pili wa umri wa miaka saba. Bomoa madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako na kuvunja sanamu ya Ashera iliyo karibu nayo. Halafu, unijengee mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, madhabahu nzuri juu ya mwinuko huu. Kisha unitolee sadaka ya kuteketezwa ya yule fahali wa pili ukitumia kuni za ile sanamu ya Ashera uliyoivunja.” Basi, Gideoni akachukua watumishi wake kumi, akafanya kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu. Lakini kwa kuwa aliiogopa jamaa yake na watu wa mjini, badala ya kufanya hayo mchana, alifanya wakati wa usiku. Wakazi wa mji walipoamka asubuhi na mapema waliona madhabahu ya Baali na sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo vimeharibiwa. Yule fahali wa pili alikuwa ameteketezwa juu ya madhabahu iliyokuwa imejengwa mahali hapo. Wakaulizana, “Nani amefanya jambo hili?” Walipofanya uchunguzi wakagundua kwamba Gideoni mwana wa Yoashi ndiye aliyekuwa amefanya hayo. Wakazi wa mji wakamjia Yoashi, wakamwambia, “Mtoe mwanao tumuue, maana ameharibu madhabahu ya Baali na kuivunja sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.” Yoashi akawaambia wale wote waliomkabili, “Je, mnamtetea Baali? Je, mtamwokoa? Yeyote atakayemtetea atauawa kabla ya mapambazuko. Kama Baali ni mungu, basi, na ajitetee mwenyewe maana madhabahu yake imebomolewa.” Siku hiyo wakamwita Gideoni “Yerubaali” maana yake, “Baali na ajitetee mbele yake”, maana aliibomoa madhabahu ya Baali. Wamidiani, Waamaleki na watu wote wanaokaa kando ya mto Yordani wakapiga kambi zao katika bonde la Yezreeli. Lakini roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Gideoni. Gideoni akapiga tarumbeta kuwaita Wabiezeri waje kumfuata. Akatuma wajumbe katika nchi yote ya Manase waje kumfuata. Wajumbe wengine akawatuma kuwaita watu wa makabila ya Asheri, Zebuluni na Naftali, nao wakaja kujiunga naye. Gideoni akamwambia Mungu, “Ikiwa utaikomboa Israeli kwa mkono wangu kama ulivyosema, sasa naweka ngozi ya kondoo kwenye sakafu ya kupuria ngano. Ikiwa kutakuwa na umande juu ya ngozi tu, na sakafu inayoizunguka ikawa kavu, basi, nitajua kuwa utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu kama ulivyosema.” Ikawa hivyo, kwa maana alipoamka asubuhi kesho yake, alikamua umande uliokuwa juu ya ile ngozi, akajaza bakuli. Gideoni akamwambia Mungu, “Tafadhali usinikasirikie. Nakuomba niseme mara moja tena. Nakuomba uniruhusu nitumie ngozi hii kufanya jaribio lingine. Nakuomba juu ya ngozi kuwe kukavu, lakini kwenye sakafu kuwe na umande.” Mungu akafanya hivyo usiku huo, maana, juu ya ngozi kulikuwa kukavu na kwenye sakafu kulikuwa na umande. Yerubaali, yaani Gideoni na watu wote waliokuwa pamoja naye waliamka mapema, wakapiga kambi yao bondeni karibu na chemchemi ya Harodi; kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini mwao bondeni karibu na mlima More. Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Watu ulio nao ni wengi mno kwangu mimi kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Waisraeli wasije wakajisifu mbele yangu na kusema kwamba wamejiokoa kwa nguvu zao wenyewe. Sasa watangazie watu wote kwamba mtu yeyote aliye mwoga au anayetetemeka arudi nyumbani kwake.” Basi, Gideoni aliwajaribu, na watu 22,000 wakarudi nyumbani akabaki na watu 10,000. Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Watu hao bado ni wengi mno. Sasa wapeleke mtoni, nami nitawajaribu huko. Mtu yeyote nitakayekuambia, ‘Huyu atakwenda nawe, huyo aende nawe. Lakini mtu yeyote nitakayekuambia hatakwenda nawe, huyo asiende nawe.’” Basi, Gideoni akawapeleka watu mtoni na Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Watu watakaoramba maji kama mbwa, utawatenganisha na wale watakaopiga magoti kunywa maji.” Idadi ya waliokunywa maji kwa kuchota kwa mikono yao na kuramba kama mbwa ilikuwa 300. Lakini wengine wote waliobaki walipiga magoti kunywa maji. Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Kwa hao watu 300 waliokunywa kwa kuramba kama mbwa, nitawaokoa Waisraeli na kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Lakini wale wengine wote warudi makwao.” Basi, Gideoni akachukua vyakula vya wale waliokuwa wanaondoka na tarumbeta, akawaaga waende makwao. Yeye akabaki na wale watu 300. Kambi ya Wamidiani ilikuwa bondeni upande wao wa chini. Usiku huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Nenda ukawashambulie kambini mwao, maana nimewatia mikononi mwako. Lakini kama unaogopa, nenda pamoja na mtumishi wako Pura. Huko utasikia wanayosema, nawe utapata nguvu za kuweza kwenda kuwashambulia.” Basi, Gideoni akaenda pamoja na mtumishi wake Pura mpaka kwenye vituo vya walinda zamu wa kambi ya Wamidiani. Wamidiani, Waamaleki na watu wote wa Mashariki walilala bondeni, wengi kama nzige, na ngamia wao wasiohesabika, wengi kama mchanga wa pwani. Gideoni alipofika, akamsikia mtu mmoja akimsimulia mwenzake ndoto yake hivi: “Niliota ndoto. Niliona mkate wa shayiri ukivingirika hadi kambini mwa Wamidiani, ukalipiga hema na kulipindua chini juu. Hema likalala chini.” Mwenzake akamjibu, “Hiyo inamaanisha tu upanga wa yule Mwisraeli Gideoni mwana wa Yoashi ambaye mikononi mwake Mungu amewatia Wamidiani pamoja na jeshi lote.” Gideoni aliposikia masimulizi hayo ya ndoto na tafsiri yake, alimwabudu Mungu. Kisha alirudi kwenye kambi ya Waisraeli, akasema, “Amkeni twende; maana Mwenyezi-Mungu amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.” Basi akawagawa wale watu 300 katika makundi matatu, akawapa tarumbeta na magudulia yenye mienge. Akawaambia, “Mniangalie na kufanya sawa kama nitakavyofanya wakati nitakapofika kambini. Nitakapopiga tarumbeta, mimi pamoja na kundi langu, nyote pigeni tarumbeta kutoka kila upande na kusema kwa sauti kubwa, ‘Kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kwa ajili ya Gideoni!’” Ilipokaribia usiku wa manane, Gideoni na kundi lake la watu mia moja mara tu baada ya kufika mwisho wa kambi, mwanzoni mwa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu walikaribia kambi ya adui. Wakapiga tarumbeta na kuvunja magudulia waliyokuwa nayo. Makundi yote matatu kwa pamoja yakapiga tarumbeta na kuvunja magudulia yao. Katika mikono yao ya kushoto walishika mienge na kwa mikono yao ya kulia tarumbeta na kuzipiga, huku wakisema kwa sauti kubwa, “Upanga kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kwa ajili ya Gideoni!” Wakasimama kila mmoja mahali pake kuizunguka kambi. Jeshi lote la adui likatawanyika huku likipiga mayowe. Watu wa Gideoni walipopiga tarumbeta zao 300, Mwenyezi-Mungu aliwafanya Wamidiani waanze kuuana wao kwa wao kambini. Waliosalia wakatoroka hadi Serera panapoelekea Beth-shita, hadi mpakani mwa Abel-mehola karibu na Tabathi. Waisraeli wa kabila la Naftali, Asheri, na Manase, wote waliitwa, wakawafuatia Wamidiani. Gideoni akatuma wajumbe kote katika nchi ya milima ya Efraimu watangaze: “Teremkeni kuwakabili Wamidiani na kuwazuia kwa kuteka vijito na mto Yordani mpaka Beth-bara.” Basi, wanaume wote wa Efraimu wakaja na kuuteka mto Yordani mpaka Beth-bara. Wakachukua mateka viongozi wawili wa Midiani, yaani Orebu na Zeebu. Wakamuua Orebu katika mwamba wa Orebu, naye Zeebu wakamuua katika shinikizo la Zeebu, wakiwa wanawafuatia Wamidiani. Wakamletea Gideoni vichwa vya Orebu na Zeebu, ngambo ya mto Yordani. Watu wa kabila la Efraimu wakamwuliza Gideoni, “Kwa nini umetutendea hivyo? Kwa nini hukutuita ulipokwenda kupigana na Wamidiani?” Wakamlaumu kwa ukali. Lakini Gideoni akawajibu, “Mambo niliyofanya mimi si kitu kabisa kama yakilinganishwa na yale mliyoyafanya nyinyi. Walichookota watu wa Efraimu baada ya mavuno ni chema na kizuri kuliko mavuno ya jamaa yangu ya Abiezeri. Mungu amewatia mikononi mwenu wakuu wa Midiani, Orebu, na Zeebu. Je, mimi nimefanya nini nikilinganishwa nanyi?” Gideoni alipokwisha sema hivyo, hasira yao dhidi yake ikatulia. Gideoni na wenzake 300 wakafika Yordani, wakavuka. Ingawa walikuwa wamechoka sana, waliendelea kuwafuatia adui zao. Basi, akawaambia watu wa Sukothi, “Tafadhali wapeni wenzangu hawa mikate maana wamechoka sana; nami bado ninaendelea kuwafuatia wafalme Zeba na Salmuna wa Midiani.” Lakini viongozi wa Sukothi wakamwuliza, “Kwa nini tuwape mikate nanyi bado hamjamshinda Zeba na Salmuna?” Gideoni akawaambia, “Sawa, lakini Mwenyezi-Mungu atakapowatia Zeba na Salmuna mikononi mwangu, nitaichanachana miili yenu kwa miiba na mbigili za jangwani.” Kutoka huko akawaendea watu wa Penueli, akawaomba namna ileile. Nao watu wa Penueli wakamjibu kama walivyomjibu watu wa Sukothi. Gideoni akawaambia, “Nitakaporudi kwa amani nitaubomoa mnara huu.” Zeba na Salmuna walikuwa huko Karkori pamoja na jeshi lao la watu 15,000 ambao ndio tu waliobaki kutoka jeshi la mashariki, maana wenzao 120,000 waliuawa. Gideoni akafuata njia ya magharibi iliyo mashariki mwa Noba na Yogbeha, akalishambulia jeshi hilo ambalo halikuwa tayari. Wafalme wa Midiani, Zeba na Salmuna walitoroka wakakimbia, lakini Gideoni aliwafuatia, akawakamata na kulitia jeshi lote hofu kubwa. Kisha, Gideoni, mwana wa Yoashi, akarudi kutoka vitani akipitia kwenye mteremko wa Heresi. Akamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumhoji. Kijana huyo akamwandikia majina ya viongozi na wazee mashuhuri wa Sukothi, jumla yao watu sabini na saba. Gideoni akarudi kwa watu wa Sukothi, akawaambia, “Si mtakumbuka mlivyonitukana mliposema, ‘Kwa nini tuwape mikate watu wako waliochoka sana nanyi bado hamjamshinda Zeba na Salmuna?’ Haya basi, Zeba na Salmuna ndio hawa.” Basi, akawachukua wazee wa Sukothi na kuwapa funzo wanaume wote kwa kuichana miili yao kwa miiba na mbigili. Vilevile akaubomoa mnara wa Penueli na kuwaua wakazi wa mji huo. Kisha, akawauliza Zeba na Salmuna, “Watu wale mliowaua huko Tabori walikuwaje?” Wakamjibu, “Walifanana na wewe, maana walionekana kama wana wa mfalme.” Naye akawaambia, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu mzazi. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kama msingewaua, hata mimi nisingewaua.” Kisha akamwambia Yetheri, mzaliwa wake wa kwanza, “Simama, uwaue.” Lakini Yetheri aliogopa kuchukua upanga wake maana alikuwa bado kijana. Hapo Zeba na Salmuna wakasema, “Tuue wewe mwenyewe, maana hii ni kazi ya mtu mzima.” Gideoni akawaua yeye mwenyewe na kuchukua mapambo yao yaliyokuwa shingoni mwa ngamia wao. Kisha, Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Wewe na uwe mtawala wetu, na baada yako watutawale wazawa wako, kwa kuwa wewe umetukomboa kutoka kwa Wamidiani.” Gideoni akawajibu, “Mimi sitakuwa mtawala wenu wala mwanangu hatakuwa mtawala wenu. Mwenyezi-Mungu ndiye atakayekuwa mtawala wenu.” Kisha akawaambia, “Ningependa kuwaomba kitu kimoja; naomba kila mmoja wenu anipe vipuli mlivyoteka nyara.” Wale Wamidiani kwa vile walikuwa Waishmaeli, walivaa vipuli vya dhahabu. Watu wakamjibu, “Tutakupa kwa hiari.” Wakatandaza nguo na kila mmoja akatupa humo vipuli walivyokuwa wameteka nyara. Uzito wa vipuli vyote alivyowataka wampe ulikuwa kilo ishirini. Zaidi ya hivyo, alipokea pia herini, mavazi ya urujuani yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani na mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia wao. Gideoni akazitumia kutengenezea kizibao ambacho alikiweka kwenye mji wake wa Ofra. Waisraeli wote wakaenda huko kukiabudu. Kizibao hicho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake. Basi, Wamidiani walishindwa kabisa wasiwe tishio kwa Israeli; na nchi ya Israeli ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini. Gideoni, yaani Yerubaali, mwana wa Yoashi akarudi nyumbani kwake na kukaa huko. Gideoni alikuwa na watoto wa kiume sabini, maana alioa wanawake wengi. Alikuwa na suria huko Shekemu ambaye alimzalia mtoto wa kiume, jina lake Abimeleki. Gideoni, mwana wa Yoashi, akafariki akiwa na umri mkubwa, akazikwa katika kaburi la Yoashi, baba yake, kwenye mji wa Ofra wa Wabiezeri. Mara baada ya kifo cha Gideoni, Waisraeli wakairudia miungu ya Baali na kuiabudu. Wakamfanya Baal-berithi kuwa mungu wao. Waisraeli wakamsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, aliyewakomboa kutoka kwa maadui zao wengi waliowazunguka kila upande. Tena, hawakuitendea wema jamaa ya Yerubaali yaani Gideoni kwa mema yote aliyoyatenda katika Israeli. Abimeleki, mwana wa Gideoni, akawaendea ndugu na wana wote wa kabila za mama yake huko Shekemu, akawaambia, “Semeni papa hapa mbele ya wananchi wote wa Shekemu: Lipi ni jema kwenu, kwamba watoto wote sabini wa kiume wa Yerubaali wawatawale au mtoto mmoja? Kumbukeni kuwa mimi ni damu yenu.” Ndugu za mama yake wakatangaza maneno haya kote Shekemu kwa niaba yake, na watu wote wa Shekemu wakaamua kumfuata maana alikuwa ndugu yao. Wakampa vipande sabini vya fedha vilivyokuwa kwenye nyumba ya Baal-berithi ambavyo alivitumia kuwakodi watu wakorofi na watu ovyoovyo ili wamfuate. Akafuatana nao kwenda Ofra kwa baba yake na huko akawaua ndugu zake wote sabini juu ya jiwe moja. Lakini Yothamu, mwana mdogo wa Yerubabeli alinusurika, maana alijificha. Wananchi wote wa Shekemu na Beth-milo wakakusanyika kwenye mwaloni ulio karibu na mnara huko Shekemu, wakamfanya Abimeleki kuwa mfalme wao. Yothamu alipopata habari hizo, alikwenda kusimama juu ya mlima Gerizimu, akasema kwa sauti kubwa, “Nisikilizeni, enyi watu wa Shekemu kama mnataka Mungu awasikilize na nyinyi. Siku moja, miti ilikwenda kujitafutia mfalme. Basi, ikauambia mzeituni, ‘Tawala juu yetu!’ Lakini mzeituni ukajibu, ‘Mnadhani naweza kuacha shughuli yangu ya kuzalisha mafuta ambayo huthaminiwa sana na miungu na wanadamu niende kujisumbua kuitawala miti?’ Kisha miti ikauambia mtini, ‘Njoo wewe utawale juu yetu.’ Lakini mtini ukajibu, ‘Je, mnadhani naweza kuacha shughuli yangu ya kuzalisha matunda mazuri na matamu, niende kujisumbua kuitawala miti?’ Halafu miti ikauambia mzabibu, ‘Njoo wewe uwe mtawala juu yetu.’ Lakini mzabibu ukajibu, ‘Mnadhani naweza kuacha shughuli yangu ya kuzalisha divai ambayo hufurahisha miungu na wanadamu, niende kujisumbua kuitawala miti?’ Mwishowe miti yote ikauendea mti wa miiba na kuuambia, ‘Njoo wewe utawale juu yetu.’ Mti wa miiba ukajibu, ‘Kama kweli mnataka kuniteua kuwa mfalme, njoni mkae chini ya kivuli changu. Lakini kama hamtaki kufanya hivyo, basi moto na utoke kwenye miiba yangu na kuiteketeza hata mierezi ya Lebanoni.’” Yothamu akaendelea kusema, “Sasa basi, mnadhani mmefanya Abimeleki mfalme kwa nia njema na uaminifu? Je, mnadhani mmemtendea wema Yerubaali na jamaa yake kama alivyostahili kwa matendo yake? Aghalabu baba yangu alihatarisha maisha yake kwa kuwapigania na kuwakomboa kutoka kwa Wamidiani! Lakini leo mmeishambulia jamaa ya baba yangu na kuwaua wana sabini juu ya jiwe moja, halafu mmemfanya Abimeleki mtoto wa mjakazi wa baba, awe mfalme wa wakazi wa Shekemu kwa sababu tu ni mtu wa ukoo wenu. Sasa basi, kama mmetenda hayo kwa nia njema na kwa kumheshimu Yerubaali na jamaa yake, basi, furahini pamoja na Abimeleki, naye afurahi pamoja nanyi. Lakini, kama sivyo, moto na utoke kwa Abimeleki na kuwateketeza wananchi wa Shekemu na Beth-milo, tena moto utoke kwa wananchi wa Shekemu na Beth-milo na kumteketeza Abimeleki.” Kisha Yothamu akatoroka, akakimbilia Beeri, akakaa huko, kwa maana alimwogopa Abimeleki ndugu yake. Akakaa huko. Abimeleki alitawala juu ya Israeli kwa muda wa miaka mitatu. Kisha Mungu akaleta roho ya uadui kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu, nao wakamwasi. Ndivyo walivyoadhibiwa watu wa Shekemu pamoja na ndugu yao Abimeleki kwa ukatili waliowafanyia wana sabini wa Yerubaali. Adhabu ya mauaji hayo iliwapata maana Abimeleki aliwaua akisaidiwa na hao watu wa Shekemu. Watu wa Shekemu waliweka washambulizi wamwotee Abimeleki kutoka vilele vya mlima. Watu hao waliwanyanganya mali zao wote waliopita huko. Abimeleki akaambiwa mambo hayo. Siku moja Gaali, mwana wa Ebedi, pamoja na ndugu zake alikwenda kukaa Shekemu. Watu wa Shekemu wakawa na imani naye. Wakatoka na kwenda kwenye mashamba yao ya mizabibu, wakachuma zabibu halafu wakazisindika, wakatengeneza divai wakafanya sikukuu. Wakaingia kwenye nyumba ya mungu wao wakala na kunywa; kisha wakamtukana Abimeleki. Gaali, mwana wa Ebedi, akasema, “Abimeleki ni nani? Sisi hapa Shekemu ni watu wa aina gani hata tumtumikie Abimeleki? Gideoni na Zebuli ofisa wake walimtumikia Hamori baba wa Shekemu, lakini kwa nini basi, sisi tumtumikie Abimeleki? Kama watu hawa wangekuwa chini yangu, ningemwondoa Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ongeza jeshi lako, kisha, njoo hadharani tupigane.’” Zebuluni, mtawala wa mji, aliposikia maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, alikasirika sana. Basi akampelekea ujumbe Abimeleki huko Torma akasema, “Gaali, mwana wa Ebedi, pamoja na ndugu zake wameingia mjini Shekemu na kuchochea uasi dhidi yako. Basi, rudi wewe na watu ulio nao, wakati wa usiku, uvizie mashambani karibu na mji. Mara jua litakapotoka wakati wa asubuhi, ushambulie mji. Gaali akitoka pamoja na watu wake kuja kukukabili, uwatendee ifaavyo.” Abimeleki aliondoka na watu waliokuwa pamoja naye kuja Shekemu wakati wa usiku. Aliwagawa watu wake katika vikosi vinne na kuvizia huko karibu na mji. Gaali, mwana wa Ebedi, akatoka nje na kusimama kwenye lango la mji, wakati huo Abimeleki na watu wake walitoka mahali walipokuwa wanavizia. Gaali alipomwona akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka vilele vya mlima.” Zebuli akamwambia, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.” Gaali akasema tena, “Tazama! Watu wanashuka katikati ya nchi na kikosi kingine kinatoka upande wa Mwaloni wa Waaguzi.” Kisha Zebuli akamwambia, “Majivuno yako yako wapi sasa? Si ni wewe uliyesema, ‘Abimeleki ni nani? Kwa nini tumtumikie?’ Sasa, hao ndio watu uliowadharau; nenda ukapigane nao.” Gaali akatoka akiwaongoza watu wa Shekemu na kupigana na Abimeleki. Gaali akashindwa na kukimbia, huku anafuatiwa na Abimeleki. Watu wengi walijeruhiwa na kuanguka njiani hadi kwenye lango la mji. Abimeleki akakaa Aruma na Zebuli akamfukuza Gaali na ndugu zake kutoka mji wa Shekemu. Siku iliyofuata, Abimeleki alipata habari kwamba watu wa Shekemu wametoka mjini na kwenda mashambani. Akachukua watu wake akawagawa katika vikosi vinne, ili waende kuvizia mashambani. Alipowaona watu wanatoka mjini, akatoka alikojificha akawaua. Abimeleki na kundi lake wakaenda mbio kwenda kulinda lango la mji. Makundi yake mawili mengine yaliwashambulia wale waliokuwa mashambani na kuwaua. Abimeleki alipigana na wakazi wa mji huo siku nzima. Akauteka mji na kuwaua watu wote waliokuwamo humo. Akauteketeza mji kwa moto na kuutia chumvi. Watu wote waliokuwa katika mnara wa Shekemu waliposikia habari hizo, walikimbilia kwenye ngome ya nyumba ya mungu aliyeitwa El-berithi. Abimeleki akaambiwa kuwa watu wote waliokuwa kwenye mnara wa Shekemu wamejikusanya pamoja. Abimeleki na watu wake wakaenda mlimani Salmoni, akachukua shoka akakata tawi la mti na kuliweka begani mwake. Halafu akawaambia wale watu aliokuwa nao waharakishe kufanya kama alivyofanya. Kila mmoja akakata tawi kama lile la Abimeleki. Wakachukua matawi yao na kuyaegemeza kwenye kuta za ngome, wakayatia moto na kuichoma ngome; watu wote wanaume na wanawake wapatao 1,000 waliokuwa katika mnara wa Shekemu wakafa. Kisha Abimeleki akaenda Thebesi, akauzingira na kuuteka. Lakini kulikuwa na mnara imara katikati ya mji. Basi, wakazi wote wa mji huo wanaume na wanawake wakakimbilia humo na kujifungia ndani. Wakapanda kwenye paa la mnara huo. Abimeleki aliufikia mnara na kuushambulia, kisha, aliukaribia mlango wa mnara autie moto. Naye mwanamke mmoja akatupa jiwe la juu la kusagia, akamponda Abimeleki kichwa. Kisha Abimeleki akamwita haraka kijana wake aliyembebea silaha akamwambia, “Chukua upanga wako uniue, wasije watu wakasema kuwa niliuawa na mwanamke.” Kijana akachukua upanga wake, akamchoma na kumuua. Waisraeli walipoona kwamba Abimeleki amekufa, wakaondoka na kurudi kila mmoja nyumbani kwake. Hivyo ndivyo Mungu alivyomwadhibu Abimeleki kwa kosa lake dhidi ya baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini. Vilevile Mungu aliwafanya watu wa Shekemu waadhibiwe kwa uovu wao walioufanya. Hivyo, laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawapata. Baada ya kifo cha Abimeleki, Tola mwana wa Pua mwana wa Dodo, wa kabila la Isakari, akatokea kuwakomboa Waisraeli. Tola aliishi Shamiri katika nchi ya milima ya Efraimu. Alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini na mitatu, kisha akafariki na kuzikwa huko Shamiri. Baada ya Tola, alitokea Yairi wa Gileadi, akawa mwamuzi wa Waisraeli kwa miaka ishirini na miwili. Yairi alikuwa na watoto wa kiume thelathini ambao walipanda punda thelathini na walikuwa na miji thelathini katika nchi ya Gileadi, ambayo mpaka leo inaitwa Hawoth-yairi. Yairi alifariki na kuzikwa huko Kamoni. Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu wakatumikia Mabaali, Maashtarothi, na miungu ya Shamu, ya Sidoni, ya Moabu, ya Amoni na ya Wafilisti. Walimwacha Mwenyezi-Mungu na wala hawakumwabudu tena. Hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa Wafilisti na Waamoni. Kwa miaka kumi na minane hao waliwatesa na kuwakandamiza Waisraeli walioishi huko Gileadi katika eneo la Waamori mashariki ya mto Yordani. Waamoni nao walivuka mto Yordani kupigana na makabila ya Yuda, Benyamini na Efraimu. Nao Waisraeli wakapata taabu sana. Basi wakamlilia Mwenyezi-Mungu, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi yako, maana tumekuacha wewe Mungu wetu, tukatumikia Mabaali.” Naye Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Je, mimi sikuwakomboa kutoka kwa Wamisri, Waamoni, Waamori, Wafilisti? Wasidoni, Waamaleki na Wamidiani waliwakandamiza nanyi mkanililia, nami nikawakomboa mikononi mwao. Hata hivyo nyinyi mmeniacha, mkatumikia miungu mingine. Kwa hiyo sitawakomboeni tena. Nendeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua. Iacheni hiyo iwakomboe katika taabu zenu!” Lakini Waisraeli wakamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tumetenda dhambi. Tufanye upendavyo, lakini tunakuomba utuokoe leo.” Kisha wakaitupilia mbali miungu ya kigeni, wakamtumikia tena Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu hakuweza kuvumilia zaidi kuona taabu za Waisraeli. Waamoni wakajikusanya wakapiga kambi yao huko Gileadi. Waisraeli nao wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Mizpa. Waisraeli na viongozi wao wakaulizana, “Ni nani atakayeanza kupigana na Waamoni? Atakayefanya hivyo ndiye atakayekuwa kiongozi wa wakazi wote wa Gileadi.” Huko Gileadi kulikuwa na mpiganaji hodari aitwaye Yeftha, mwana wa mama mmoja malaya, na baba yake aliitwa Gileadi. Gileadi alikuwa pia na wana wengine kwa mke wake wa halali. Watoto wa mke huyo walipokuwa wakubwa, walimfukuza Yeftha kutoka nyumbani, wakamwambia, “Wewe huna haki ya kupata urithi kutoka kwa baba yetu, maana wewe ni mtoto wa mwanamke mwingine.” Basi, Yeftha akawakimbia ndugu zake akaenda kuishi katika nchi ya Tobu. Huko watu ovyo wakakusanyika kujiunga naye, wakamfuata katika safari zake za mashambulio. Baada ya muda fulani, Waamoni waliwashambulia Waisraeli. Wakati vita vilipopamba moto, wazee wa Gileadi wakaenda kumleta Yeftha kutoka nchi ya Tobu, wakamwambia, “Njoo utuongoze katika vita vyetu na Waamoni.” Lakini Yeftha akawaambia hao wazee wa Gileadi, “Je, si mlinichukia hata mkanifukuza kutoka kwa jamaa ya baba yangu? Kwa nini mnanijia sasa mkiwa katika taabu?” Hao wazee wa Gileadi wakamwambia “Ndio maana tumekujia ili uende nasi kupigana na Waamoni, nawe utakuwa kiongozi wetu na wa wakazi wote wa Gileadi.” Yeftha akawaambia hao wazee wa Gileadi, “Kama mkinirudisha nyumbani kupigana na Waamoni halafu Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwangu, mimi nitakuwa kiongozi wenu.” Wale wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, “Mwenyezi-Mungu atakuwa shahidi kati yetu. Hakika tutafanya kama ulivyosema.” Yeftha akafuatana na wazee wa Gileadi, nao watu wakamfanya kiongozi wao. Yeftha akasema masharti yake huko Mizpa mbele ya Mwenyezi-Mungu Yeftha akapeleka ujumbe kwa mfalme wa Amoni akamwambia, “Una ugomvi gani nasi hata uje kuishambulia nchi yetu?” Mfalme wa Amoni akawajibu hao wajumbe, “Waisraeli walipotoka Misri, walichukua nchi yangu kutoka mto Arnoni hadi mto Yaboki na mto Yordani. Sasa nirudishie nchi hiyo kwa amani.” Yeftha akatuma tena wajumbe kwa mfalme wa Amoni wamwambie kwa niaba yake, “Waisraeli hawakuchukua nchi ya Wamoabu wala nchi ya Waamoni. Lakini Waisraeli walipotoka Misri, walisafiri jangwani hadi bahari ya Shamu mpaka Kadeshi. Kisha Waisraeli wakatuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu wakimwomba awaruhusu kupita katika nchi yake, lakini mfalme wa Edomu akakataa. Basi wakamwomba ruhusa mfalme wa Moabu naye pia akakataa. Kwa hiyo Waisraeli wakabaki Kadeshi. Kisha wakasafiri wakipitia jangwani kuzunguka nchi ya Edomu na Moabu mpaka walipofika upande wa mashariki wa Moabu, wakapiga kambi ngambo ya mto Arnoni. Lakini hawakuingia eneo la Moabu. Mto Arnoni ndio uliokuwa mpaka wa Moabu. Hapo Waisraeli walituma wajumbe kwa mfalme Sihoni wa Waamori huko Heshboni wakamwomba awaruhusu kupita katika nchi yake waende katika nchi yao. Lakini Sihoni hakuwakubali Waisraeli wapite katika nchi yake. Basi, Sihoni akakusanya watu wake wote, akapiga kambi huko Yahasa, akawashambulia Waisraeli. Naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni pamoja na watu wake mikononi mwa Waisraeli, wakawashinda. Hivyo Waisraeli wakachukua nchi yote ya Waamori ambao walikuwa wanaishi huko. Walilichukua eneo lote la Waamori tangu mto Arnoni hadi mto Yaboki na tangu jangwani upande wa mashariki hadi mto Yordani magharibi. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akawafukuza Waamori mbele ya Waisraeli. Je, wewe unataka kutunyanganya nchi yetu? Tosheka na kile ambacho mungu wako Kemoshi amekupa. Lakini nchi yoyote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, amewafukuza wakazi wake, akatupa sisi, hiyo ni mali yetu sisi. Je, unadhani wewe una nguvu kuliko Balaki mwana wa Zipora aliyekuwa mfalme wa Moabu? Yeye hakushindana na Waisraeli au kupigana nao. Wakati wote Waisraeli walipoishi mjini Heshboni na vijiji vyake, na mji wa Aroeri na vijiji vyake pamoja na miji yote iliyo ukingoni mwa mto Arnoni kwa muda wa miaka 300, kwa nini hukulikomboa eneo hilo wakati huo? Mimi sijakukosea kitu na ndio maana unafanya kosa unaponishambulia. Mwenyezi-Mungu ambaye ndiye Mwamuzi ataamua leo hii kati ya Waisraeli na watu wa Amoni.” Lakini mfalme wa Amoni alipuuza ujumbe huo wa Yeftha. Kisha roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Yeftha, naye akaondoka na kupitia Gileadi na Manase, akarudi Mizpa katika nchi ya Gileadi na kuendelea hadi Amoni. Yeftha akamwapia Mwenyezi-Mungu akisema, “Kama utawatia Waamoni mikononi mwangu, basi, yeyote atakayetoka nje kutoka nyumbani mwangu kuja kunilaki nitakapokuwa narudi baada ya kuwashinda Waamoni, huyo atakuwa wako wewe Mwenyezi-Mungu. Huyo nitakutolea sadaka ya kuteketezwa.” Basi, Yeftha akavuka mto, akapigana na Waamoni, naye Mwenyezi-Mungu akawatia Waamoni mikononi mwake. Akajipatia ushindi mkubwa, akateka maeneo ishirini yaliyokuwa kati ya Aroeri, sehemu zilizozunguka Minithi na Abel-keramimu. Basi Waamoni wakashindwa kabisa na Waisraeli. Yeftha alipokuwa anarudi nyumbani kwake huko Mizpa, binti yake akatoka kuja kumlaki akicheza na kupiga matari. Msichana huyo alikuwa ndiye mtoto wake wa pekee. Yeftha hakuwa na mtoto mwingine wa kiume wala wa kike. Yeftha alipomwona, alirarua mavazi yake kwa huzuni na kusema, “O binti yangu! Umenivunja moyo. Wewe umekuwa chanzo kikubwa cha matatizo kwangu. Nimekwisha mwapia Mwenyezi-Mungu nami siwezi kuvunja kiapo changu.” Naye akamwambia, “Baba, kama umemwapia Mwenyezi-Mungu kitu, basi nitendee kama ulivyoahidi, kwa vile sasa amekuwezesha kuwalipiza kisasi adui zako Waamoni.” Kisha, akamwambia baba yake, “Nakuomba jambo hili moja, nipatie muda wa miezi miwili, niende na rafiki zangu milimani, niomboleze kufariki kwangu kabla ya kuolewa.” Baba yake akamruhusu aende huko kwa miezi miwili. Naye akaenda pamoja na rafiki zake, wakaomboleza kufa kwake kabla ya kuolewa. Baada ya miezi miwili akarudi nyumbani; kisha baba yake akamtendea kulingana na nadhiri yake. Msichana huyo hakuwa amemjua mwanamume yeyote. Basi, tangu wakati huo kukawa na desturi hii katika Israeli: Kila mwaka wanawake wa Israeli huenda kuomboleza kwa siku nne kifo cha bintiye Yeftha wa Gileadi. Watu wa kabila la Efraimu walikusanyika, wakavuka mto Yordani wakafika huko Zafoni. Kisha wakamwambia Yeftha, “Kwa nini hukutuita tuende pamoja nawe kupigana na Waamoni? Sasa tutaichoma nyumba yako nawe mwenyewe ndani yake.” Yeftha akawaambia, “Mimi pamoja na watu wangu tulikuwa na uadui mkubwa na Waamoni. Niliwaombeni mnisaidie lakini hamkuja kuniokoa. Nilipoona kwamba hamkuja kuniokoa, nilikwenda, roho mkononi, kupigana na Waamoni, naye Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwangu. Kwa nini sasa mnakuja kupigana na mimi?” Basi, Yeftha akakusanya watu wote wa Gileadi, akapigana na watu wa Efraimu. Watu wa Gileadi wakawashinda watu wa Efraimu. Hawa Waefraimu ndio hao waliokuwa wamesema: “Nyinyi watu wa Gileadi ni wakimbizi wa kabila la Efraimu mliotoka katika kabila la Efraimu mkaenda kwa kabila la Manase.” Kisha watu wakavishika vivuko vya mto Yordani ili kuiziba njia ya watu wa Efraimu. Kila mara alipotokea mkimbizi akaomba kupita huko, watu wa Gileadi walimwuliza, “Je, wewe ni Mwefraimu?” Na kama alijibu, “La,” walimwambia: “Haya tamka neno ‘Shibolethi’” lakini yeye hutamka “Sibolethi,” kwa sababu hakuweza kulitamka sawasawa. Hapo, walimkamata, wakamuua huko kwenye vivuko vya mto Yordani. Watu 42,000 wa Efraimu walipoteza maisha yao wakati huo. Yeftha alikuwa mwamuzi katika Israeli kwa miaka sita. Kisha akafariki, akazikwa huko Gileadi katika mji wake. Baada ya Yeftha, Ibzani kutoka Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli. Yeye alikuwa na watoto wa kiume thelathini na wa kike thelathini. Nao binti zake thelathini aliwaoza nje ya ukoo wake, na wana aliwaoza wasichana thelathini kutoka nje ya ukoo wake. Ibzani alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka saba. Akafariki, akazikwa mjini Bethlehemu. Baada ya Ibzani, Eloni wa kabila la Zebuluni, akawa mwamuzi wa Israeli kwa miaka kumi. Naye akafariki, akazikwa mjini Aiyaloni katika nchi ya kabila la Zebuluni. Baada ya Eloni, Abdoni mwana wa Hileli kutoka Pirathoni akawa mwamuzi wa Israeli. Yeye alikuwa na watoto wa kiume arubaini na wajukuu thelathini ambao walipanda punda sabini. Alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka minane. Kisha Abdoni akafariki, akazikwa mjini Pirathoni katika nchi ya kabila la Efraimu kwenye eneo la milima ya Waamaleki. Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye akawaacha watawaliwe na Wafilisti kwa miaka arubaini. Kulikuwa na mtu mmoja huko Sora, wa kabila la Dani, jina lake Manoa. Mke wake alikuwa tasa. Siku moja, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea huyo mwanamke, akamwambia, “Wewe ni tasa, huna watoto. Lakini utapata mimba na kumzaa mtoto wa kiume. Kwa hiyo uwe mwangalifu, usinywe divai au kileo wala usile kitu chochote kilicho najisi, kwa maana utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Nywele za mtoto huyo kamwe zisinyolewe, maana atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake. Naye ataanza kuwakomboa Waisraeli mikononi mwa Wafilisti.” Mwanamke huyo akaenda kumwambia mume wake, “Mtu wa Mungu ambaye sura yake ilikuwa kama ya malaika wa Mungu alinijia. Sikumwuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake. Lakini aliniambia kwamba nitachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Aliniamuru nisinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi, maana mtoto huyo atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake mpaka atakapokufa.” Kisha Manoa akamwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Nakuomba ee Mwenyezi-Mungu, umtume tena yule mtu wako uliyemtuma ili atufundishe mambo tunayopaswa kumtendea huyo mtoto atakayezaliwa.” Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi la Manoa, na yule malaika wa Mungu akamwendea tena yule mwanamke alipokuwa ameketi shambani. Lakini mumewe, Manoa, hakuwa pamoja naye. Mwanamke akakimbia upesi, akamwambia mumewe, “Tazama! Yule mtu aliyenijia siku ile amenitokea tena.” Manoa akafuatana naye mpaka kwa mtu huyo, akamwuliza, “Je, wewe ni yule mtu aliyezungumza na mwanamke huyu?” Yule mtu akamjibu, “Ni mimi.” Kisha Manoa akasema, “Sasa maneno yako yatakapotimia ni mambo gani tutakayofuata kwa ajili ya huyo mtoto? Tutafanya nini kwa ajili yake?” Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Manoa, “Mkeo atapaswa kushika yote niliyomwambia: Asionje mazao yoyote ya mzabibu, wala asinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi. Yote niliyomwamuru, ayafuate.” Manoa akamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, “Tafadhali, ukae kidogo tukutayarishie mwanambuzi.” Yule malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Manoa, “Hata kama mkinilazimisha kukaa sitakula chakula chenu. Lakini kama ukipenda, tayarisha sadaka ya kuteketezwa, mtolee Mwenyezi-Mungu.” Manoa hakujua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu. Basi, Manoa akamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, “Tuambie jina lako ili tukuheshimu wakati maneno yako yatakapotimia.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa nini unataka kujua jina langu, kwa kuwa jina langu ni la ajabu?” Hapo Manoa akatayarisha mwanambuzi na tambiko, akaviweka juu ya mwamba amtolee Mwenyezi-Mungu afanyaye maajabu. Basi, wakati Manoa na mkewe walipokuwa wanatazama miali ya moto ikipanda juu mbinguni kutoka madhabahuni, walimwona malaika katika miali hiyo akipanda kwenda mbinguni. Basi Manoa na mkewe wakasujudu. Manoa akajua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu. Malaika hakumtokea tena Manoa na mkewe. Basi, Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, maana tumemwona Mungu.” Lakini mkewe akamjibu, “Kama Mwenyezi-Mungu angetaka kutuua hangepokea sadaka yetu ya kuteketezwa na ya nafaka; wala hangetuonesha mambo hayo wala kutuambia maagizo.” Kisha mkewe Manoa akajifungua mtoto wa kiume, naye Manoa akampa jina Samsoni. Mtoto huyo akakua naye Mwenyezi-Mungu akambariki. Roho ya Mwenyezi-Mungu ikaanza kumsukuma akiwa huko Mahane-dani, kati ya Sora na Eshtaoli. Siku moja, Samsoni aliteremka na kwenda Timna ambako alimwona msichana mmoja Mfilisti. Aliporudi nyumbani akawaambia wazazi wake, “Nimemwona msichana mmoja Mfilisti huko Timna. Niozeni msichana huyo.” Lakini wazazi wake wakamwambia, “Je, hakuna msichana yeyote miongoni mwa ndugu zako au kati ya watu wetu hata uende kuoa kwa Wafilisti wasiotahiriwa?” Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Niozeni msichana huyo, maana ananipendeza sana.” Wazazi wake hawakujua kwamba huo ulikuwa mpango wa Mwenyezi-Mungu ambaye alikuwa anatafuta kisa cha kuchukua hatua dhidi ya Wafilisti. Wakati huo, Wafilisti waliwatawala Waisraeli. Samsoni na wazazi wake waliondoka kwenda Timna. Walipofika huko kwenye mashamba ya mizabibu, mwanasimba mmoja akatokea akamngurumia Samsoni. Basi, roho ya Mwenyezi-Mungu ikamwingia Samsoni kwa nguvu, akamrarua simba huyo kama mtu araruavyo mwanambuzi. Naye Samsoni hakuwaambia wazazi wake kisa hicho. Kisha akateremka akaenda kuzungumza na yule msichana; huyo msichana alimpendeza sana Samsoni. Baada ya siku chache alirudi huko Timna kumchukua huyo msichana. Alipokuwa njiani akageuka pembeni kuuona mzoga wa yule simba, na kumbe kulikuwa na nyuki ndani ya mzoga na asali. Basi, akapakua asali kwa mikono yake akawa anakula huku akiendelea na safari yake. Aliporudi kwa wazazi wake, akawapa asali kidogo nao wakala. Lakini hakuwaambia kwamba alitoa asali hiyo ndani ya mzoga wa simba. Baba yake akaenda nyumbani kwa yule msichana, naye Samsoni akafanya karamu huko, kama walivyofanya vijana wakati huo. Wafilisti walipomwona Samsoni wakamletea vijana thelathini wakae naye. Samsoni akawaambia, “Nitatega kitendawili. Kama mkiweza kutegua kitendawili hicho kwa muda wa siku saba za sherehe za harusi, basi, nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavazi thelathini ya sikukuu. Lakini msipoweza kukitegua, nyinyi mtanipa mavazi thelathini ya kitani na mavazi thelathini ya sikukuu.” Nao wakamwambia, “Haya tega tusikie.” Samsoni akawaambia, “Kwa mla kukatoka mlo kwa mwenye nguvu, utamu.” Baada ya siku tatu hao vijana walikuwa bado hawajaweza kutegua hicho kitendawili. Basi siku ya saba wakamwambia mke wa Samsoni, “Mbembeleze mumeo ili atuambie maana ya kitendawili hicho, la sivyo tutakuteketeza kwa moto wewe pamoja na nyumba ya baba yako. Je, mlitualika hapa kuja kutunyanganya mali zetu?” Mke wa Samsoni akamwendea Samsoni, huku machozi yanamtiririka, akamwambia, “Kwa kweli unanichukia; hunipendi hata kidogo. Umewategea kitendawili watu wangu na hukuniambia maana yake.” Samsoni akamjibu, “Mimi sijawaeleza hata wazazi wangu. Sasa nitawezaje kukuambia wewe?” Lakini aliendelea kulia katika muda wao wote wa siku saba za sherehe za harusi. Siku ya saba Samsoni akamwambia mkewe kile kitendawili kwani alimbana sana. Mkewe akaenda haraka akawaambia watu wake. Siku hiyo ya saba, kabla ya jua kutua, wakamwambia Samsoni, “Ni kitu gani kitamu kuliko asali? Ni nani mwenye nguvu kuliko simba?” Samsoni akawajibu, “Kama hamngejishughulisha na mtamba wangu hamngeweza kukitegua kitendawili changu.” Hapo roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Samsoni kwa nguvu, naye akaenda mjini Ashkeloni, akawaua watu thelathini, kisha akachukua mavazi yao ya sikukuu, akawapa wale waliotegua kitendawili chake. Halafu akaondoka, akaenda nyumbani kwa wazazi wake akiwa na hasira kali. Basi, wakamwoza mwanamke wake kwa kijana mmoja ambaye alikuwa mdhamini wa Samsoni katika harusi. Baada ya muda fulani, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni alichukua mwanambuzi, akaenda kumtembelea mkewe. Akamwambia baba mkwe wake kwamba anataka kumwona mke wake chumbani mwake. Lakini baba mkwe hakumruhusu, akamwambia, “Mimi nilidhani ulimchukia kabisa. Kwa hiyo nilimwoza rafiki yako. Hata hivyo, dada yake mdogo ni mzuri kuliko yeye. Tafadhali, umwoe huyo badala yake.” Samsoni akamwambia, “Safari hii sitakuwa na lawama kwa yale nitakayowatendea Wafilisti.” Basi, Samsoni akaenda, akawakamata mbweha 300 na akawafunga mikia yao pamoja wawiliwawili. Kisha akaweka mwenge katika kila jozi ya mbweha. Halafu akaiwasha hiyo mienge na kuwaachilia hao mbweha ambao waliingia kwenye mashamba ya Wafilisti na kuteketeza miganda ya ngano na pia ngano iliyokuwa bado haijavunwa hata na mashamba ya mizeituni. Wafilisti walipotaka kujua aliyefanya hayo, waliambiwa, “Ni huyo Samsoni, mkwewe Mtimna, amefanya hivyo kwa sababu huyo baba mkwe wake amemchukua mke wake na kumwoza kwa kijana mmoja aliyekuwa mdhamini wake mwenyewe Samsoni katika harusi.” Basi Wafilisti wakaenda kumchoma moto yule mwanamke pamoja na baba yake. Samsoni akawaambia hao Wafilisti, “Kama hayo ndiyo mliyoyafanya, naapa kwamba sitaondoka mpaka nimelipiza kisasi.” Basi, akawashambulia vikali na kuwaua wengi. Kisha akaenda kuishi katika pango la mwamba wa Etamu. Wafilisti wakaja, wakapiga kambi yao nchini Yuda na kuushambulia mji wa Lehi. Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kutushambulia?” Nao wakawajibu, “Tumekuja ili tumfunge Samsoni na kumtendea kama alivyotutendea.” Basi, watu 3,000 wa Yuda wakamwendea Samsoni pangoni mwa mwamba wa Etamu wakamwambia, “Je, hujui kwamba Wafilisti wanatawala juu yetu? Tazama basi, mkosi uliotutendea!” Samsoni akawajibu, “Kama walivyonitendea ndivyo nilivyowatendea.” Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga ili tukutie mikononi mwao.” Samsoni akawaambia, “Niapieni kwamba nyinyi wenyewe hamtaniua.” Nao wakamwambia, “Sisi hatutakuua ila tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi, wakamfunga kwa kamba mbili mpya na kumtoa humo pangoni. Alipofika Lehi, Wafilisti walimwendea mbio huku wakipiga kelele. Ghafla roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Samsoni kwa nguvu na zile kamba walizomfunga mikononi mwake zikakatika kama kitani kilichoshika moto, navyo vifungo vikaanguka chini. Samsoni akapata utaya mbichi wa punda, akautumia kuwaua watu 1,000. Kisha Samsoni akasema, “Kwa utaya wa punda, nimeua watu elfu moja. Kwa utaya wa punda, nimekusanya marundo ya maiti.” Alipomaliza kusema, akatupa utaya huo. Mahali hapo pakaitwa Ramath-lehi, yaani mlima wa utaya. Kisha Samsoni akashikwa na kiu sana. Basi, akamwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Ee Mungu, wewe ndiwe uliyeleta ukombozi huu, kwa kunitumia mimi mtumishi wako. Je, sasa utaniacha nife kwa kiu na kutekwa na Wafilisti hawa wasiotahiriwa?” Mungu akafungua mahali palipokuwa na shimo huko Leki, akatiririsha maji. Samsoni akanywa maji hayo na nguvu zake zikamrudia. Chemchemi hiyo ikaitwa En-hakore; nayo iko huko Lehi mpaka leo. Samsoni alikuwa mwamuzi wa Waisraeli kwa miaka ishirini, nyakati za Wafilisti. Siku moja Samsoni alikwenda mjini Gaza, akakutana na malaya mmoja akalala naye. Watu wa Gaza walipoambiwa kuwa Samsoni yuko huko, walilizingira eneo hilo na kumvizia kwenye lango la mji usiku kucha. Wakakaa kimya huko langoni usiku wote wakifikiri kwamba wanaweza kungojea mpaka mapambazuko wapate kumuua. Lakini Samsoni akabaki mjini mpaka usiku wa manane. Wakati wa usiku wa manane akaamka akashika miimo miwili ya malango, akaingoa pamoja na makomeo yake akaibeba na kwenda nayo mpaka karibu na Hebroni. Baada ya hayo, Samsoni alimpenda mwanamke mmoja aitwaye Delila ambaye aliishi katika bonde la Soreki. Wakuu wa Wafilisti wakamjia Delila, wakamwambia, “Mbembeleze Samsoni ili ujue asili ya nguvu zake nyingi ili tuweze kumkamata na kumfunga. Ukifanya hivyo, kila mmoja wetu atakupa vipande thelathini vya fedha.” Delila akamwambia Samsoni, “Tafadhali, niambie asili ya nguvu zako, na jinsi gani mtu anaweza kukushinda na kukufunga.” Samsoni akamjibu, “Wakinifunga kwa kamba saba mbichi za upinde, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” Wakuu wa Wafilisti wakamletea Delila kamba hizo saba mbichi za upinde, naye akamfunga Samsoni kwa kamba hizo. Delila alikuwa ameweka watu wamvizie katika chumba cha ndani. Kisha, akamwambia Samsoni kwa sauti kubwa, “Samsoni, Wafilisti wamekujia kukushambulia.” Samsoni akazikata kamba hizo kama nyuzi za kitani zinapogusa moto. Hivyo hakuna aliyegundua siri ya nguvu zake. Delila akamwambia Samsoni, “Wewe umenidhihaki. Umenidanganya. Tafadhali niambie jinsi unavyoweza kufungwa.” Samsoni akamjibu, “Wakinifunga kwa kamba mpya ambazo hazijatumiwa, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” Basi, Delila akachukua kamba mpya, akamfunga nazo. Kisha akamwambia Samsoni kwa sauti kubwa, “Samsoni! Wafilisti wamekuja kukushambulia!” Wakati huo kulikuwa na watu chumbani wakimvizia. Samsoni akazikata kamba hizo kama uzi. Delila akamwambia Samsoni, “Mpaka sasa bado unanidhihaki. Umenidanganya. Niambie unavyoweza kufungwa.” Samsoni akamwambia, “Ukivisuka vishungi vyangu saba vya nywele zangu katika mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” Wakati Samsoni alipokuwa analala Delila akavisuka pamoja vishungi saba vya nywele za Samsoni akavifunga kwa mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi. Kisha akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia.” Samsoni akaamka kutoka usingizini akakingoa kile kigingi na kuutatua ule mtandio wa nguo. Delila akamwambia Samsoni, “Unawezaje kusema kuwa unanipenda na moyo wako hauko pamoja nami? Umenidhihaki sasa mara tatu. Hujaniambia asili ya nguvu zako iko wapi.” Delila alipoendelea kumbana sana Samsoni kwa maneno, siku baada ya siku na kumkera hata akachoka rohoni karibu kufa, hakuweza kuvumilia, akamfunulia siri yake, akisema, “Nywele zangu kamwe hazijapata kunyolewa. Mimi nimewekwa wakfu kwa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nikinyolewa nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” Basi, Delila alipoona kwamba Samsoni amemwambia siri yake yote, akawaita wakuu wa Wafilisti, akawaambia, “Njoni safari hii moja tu maana Samsoni ameniambia siri yake yote.” Wakuu wa Wafilisti wakamwendea Delila huku wamemletea fedha walizomwahidi. Naye Delila akamfanya Samsoni alale usingizi magotini mwake, akamwita mtu amnyoe vile vishungi vyake saba. Kisha Delila akaanza kumtesa Samsoni kwa kuwa sasa nguvu zilikuwa zimemtoka. Delila akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia!” Samsoni akaamka usingizini huku akifikiri kwamba atatoka na kujiokoa kama hapo awali. Kumbe hakujua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwacha. Wafilisti walimkamata, wakamngoa macho, wakampeleka Gaza, wakamfunga kwa pingu za shaba, na kumlazimisha kufanya kazi ya kusaga unga huko gerezani. Lakini nywele zake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa. Wakuu wa Wafilisti walikusanyika ili kusherehekea na kumtolea tambiko mungu wao aitwaye Dagoni. Basi, wakawa wanaimba, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu Samsoni.” Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao na kusema, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu ambaye amekuwa akiharibu nchi yetu na kuwaua wengi wetu.” Walipojawa na furaha sana mioyoni mwao, wakasema, “Mleteni Samsoni atutumbuize.” Basi wakamtoa Samsoni gerezani, wakamleta naye akawatumbuiza. Wakamweka katikati ya nguzo. Samsoni akamwambia kijana aliyekuwa anamwongoza, “Niruhusu nizipapase nguzo zinazotegemeza jumba hili ili nami niziegemee.” Jumba hilo lilikuwa limejaa watu: Wakuu wote wa Wafilisti walikuwapo na kwenye paa kulikuwa na watu 3,000 wanaume na wanawake, wakimtazama Samsoni akiwatumbuiza. Hapo Samsoni akamwomba Mwenyezi-Mungu: “Bwana Mwenyezi-Mungu nakuomba unikumbuke. Nitie nguvu, mara hii moja tu, ee Mungu, ili niwalipize kisasi mara moja hii tu Wafilisti ambao waliyangoa macho yangu mawili.” Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo zilitegemeza uzito wote wa jumba hilo, mkono mmoja nguzo hii na mkono mwingine nguzo ya pili. Kisha akasema, “Na nife pamoja na Wafilisti.” Akasukuma kwa nguvu zake zote. Jumba likawaangukia wakuu hao wote wa Wafilisti waliokuwamo humo ndani. Wale waliouawa wakati wa kifo chake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake. Ndugu zake na jamaa yake yote wakaja kumchukua; wakamzika katikati ya mji wa Sora na mji wa Eshtaoli katika kaburi la Manoa, baba yake. Samsoni alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini. Kulikuwa na mtu mmoja huko katika milima ya Efraimu, jina lake Mika. Siku moja alimwambia mama yake, “Vile vipande 1,100 vya fedha ulivyoibiwa, nawe ukamlaani aliyekuibia nikisikia, mimi ninavyo. Mimi ndiye niliyevichukua.” Mama yake akasema, “Mwanangu, ubarikiwe na Mwenyezi-Mungu.” Mika akamrudishia mama yake hivyo vipande 1,100 vya fedha. Mama yake akasema, “Ili laana niliyotoa isikupate, fedha hii naiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, ili kutengenezea sanamu ya kuchonga na ya kusubu. Sasa ninakurudishia vipande hivyo vya fedha.” Mika alipomrudishia mama yake hiyo fedha, mama yake akachukua vipande 200 vya fedha, akampa mfua fedha, naye akafua sanamu ya kuchonga na ya kusubu. Sanamu hiyo ikawekwa ndani ya nyumba ya Mika. Mtu huyo, Mika, alikuwa na mahali pake pa ibada. Alitengeneza kizibao cha kuhani na kinyago, kisha akamfanya mmoja wa watoto wake kuwa kuhani wake. Siku hizo hapakuwepo na mfalme katika Israeli. Kila mtu alifanya chochote alichoona ni chema. Wakati huo kulikuwa na kijana mmoja Mlawi mjini Bethlehemu nchini Yuda. Kijana huyo akaondoka Bethlehemu nchini Yuda, akaenda kutafuta mahali pengine pa kuishi. Katika safari yake akafika nyumbani kwa Mika katika nchi ya milima ya Efraimu. Mika akamwuliza, “Umetoka wapi?” Naye akamjibu, “Mimi ni Mlawi, kutoka mjini Bethlehemu nchini Yuda. Nitakaa popote nitakapopata nafasi ya kukaa kama mgeni.” Mika akamwambia, “Kaa pamoja nami, uwe kwangu kama baba na kuhani wangu. Nitakulipa vipande kumi vya fedha kila mwaka na mavazi pamoja na mahitaji yako.” Huyo Mlawi akaingia akakubali, akakaa huko na kuwa kama mmoja wa wana wa Mika. Naye Mika akamfanya kijana huyo Mlawi kuwa kuhani wake huko nyumbani kwake. Kisha akasema, “Sasa najua kwamba Mwenyezi-Mungu atanifanikisha kwani nina kijana huyu Mlawi kama kuhani wangu.” Siku hizo hakukuwa na mfalme katika Israeli. Basi kabila la Dani lilikuwa linatafuta eneo lake lenyewe la kuishi humo, kwani mpaka wakati huo, halikuwa limegawiwa sehemu yake lenyewe miongoni mwa makabila ya Israeli. Hivyo watu wa kabila la Dani walichagua miongoni mwao watu hodari wakawatuma kutoka huko Eshtaoli na Sora wakawaamuru waende kuipeleleza nchi. Basi watu hao wakafika katika nchi ya milima ya Efraimu, nyumbani kwa Mika, wakakaa humo. Walipokuwa nyumbani kwa Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi. Wakamgeukia na kumwuliza, “Nani amekuleta huku? Una shughuli gani hapa?” Yeye akawajibu, “Mika amefanya nami mpango; ameniajiri nami nimekuwa kuhani wake.” Nao wakamwambia, “Tafadhali utuulizie kwa Mwenyezi-Mungu kama tutafanikiwa katika safari yetu.” Yule kuhani akawaambia, “Nendeni kwa amani. Mwenyezi-Mungu anaichunga safari yenu.” Basi, watu hao watano wakaondoka, wakaenda Laishi. Waliwaona watu walioishi huko, na jinsi walivyokaa kwa usalama kama vile watu wa Sidoni. Walikuwa watu watulivu wasio na wasiwasi na hawakupungukiwa mahitaji yoyote nchini. Walikuwa mbali na watu wa Sidoni, na hawakuwa na shughuli yoyote na watu wengine. Basi hao wapelelezi walirudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, nao wakawauliza, “Mmetuletea taarifa gani?” Wao wakasema, “Inukeni twende na kuishambulia nchi hiyo. Tumeiona nchi hiyo, na kweli ni nchi yenye rutuba. Je, mtakaa hapa tu bila kufanya kitu? Msikawie kwenda kuimiliki nchi hiyo. Mtakapofika huko mtakuta watu wasio na wasiwasi wowote. Nchi hiyo ni kubwa, haikupungukiwa chochote na Mungu ameitia mikononi mwetu.” Basi, watu 600 wa kabila la Dani wakiwa na silaha zao za vita wakaondoka kutoka Sora na Eshtaoli wakaenda kupiga kambi yao huko Kiriath-yearimu katika nchi ya Yuda. Ndiyo maana mahali hapo, upande wa magharibi wa Kiriath-yearimu pameitwa Mahane-dani mpaka leo. Kutoka huko wakaelekea nchi ya milima ya Efraimu, wakafika nyumbani kwa Mika. Watu wale watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mnajua kwamba katika nyumba mojawapo ya hizi kuna kizibao, kinyago na sanamu ya kusubu? Basi, fikirini namna ya kufanya.” Basi wale wapelelezi wakaelekea kwenye nyumba ya Mika, wakaingia ndani na kumwuliza habari zake yule kijana Mlawi. Wakati huo, wale watu 600 wa kabila la Dani wakiwa na silaha zao za vita walisimama mlangoni. Wale watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi waliingia ndani, wakachukua ile sanamu mungu ya kusubu, kile kizibao na kinyago cha ibada. Wakati huo yule kuhani alikuwa amesimama mlangoni pamoja na wale watu 600 wenye silaha. Basi, alipowaona wale wapelelezi wameingia nyumbani mwa Mika wakachukua sanamu ya kuchonga, kifuko cha kauli, kinyago na sanamu ile ya kusubu, akawauliza, “Mnafanya nini?” Nao wakamwambia, “Nyamaza, funga mdomo wako, uje pamoja nasi, uwe kuhani wetu na kama baba yetu. Au waonaje? Je, yafaa kwako zaidi kuwa kuhani wa mtu mmoja ama kuwa kuhani wa kabila moja la Israeli?” Yule kuhani akafurahi sana akachukua kile kifuko, kile kinyago cha ibada, na ile sanamu ya mungu ya kusubu, akafuatana nao. Basi, wakaanza safari yao, huku wametanguliwa na watoto wao na mifugo na mali zao. Walipokuwa wamefika mbali na nyumbani kwa Mika, watu waliokuwa jirani na Mika wakaitwa, wakawafuatia watu wa kabila la Dani wakawafikia. Kisha wakawapigia kelele, nao watu wa kabila la Dani wakageuka, wakamwuliza Mika, “Una shida gani hata umetufuatia pamoja na kundi hili lote?” Mika akasema, “Nyinyi mmechukua miungu yangu niliyojitengenezea, mkamchukua na kuhani wangu, mkaniacha bila chochote. Mnawezaje basi kuniuliza nina shida gani?” Watu wa kabila la Dani wakamwambia, “Afadhali uache kelele zako, la sivyo wengine wetu wenye hasira wanaweza wakakuvamia, nawe ukapoteza maisha yako na maisha ya jamaa yako.” Mika alipoona kwamba wamemzidi nguvu, akageuka, akarudi nyumbani; nao watu wa kabila la Dani wakaenda zao. Hao watu wa kabila la Dani walivichukua vitu vile ambavyo Mika alikuwa amevitengeneza, wakamchukua na yule kuhani aliyemhudumia. Basi wakaenda kushambulia Laishi wakawaua wakazi wake ambao waliishi humo kwa utulivu na bila wasiwasi, wakauteketeza mji huo. Wakazi wa mji huo hawakuwa na mtu wa kuwaokoa kwa sababu walikuwa mbali na mji wa Sidoni, tena hawakuwa na uhusiano na watu wengine. Mji huo ulikuwa kwenye bonde la Beth-rehobu. Watu wa kabila la Dani wakaujenga upya, wakaishi humo. Walibadilisha jina la mji huo, wakauita Dani, kufuata jina la babu yao aliyekuwa mwana wa Israeli. Lakini mji huo hapo awali uliitwa Laishi. Watu wa kabila la Dani wakaisimika ile sanamu ya kuchonga, naye Yonathani, mwana wa Gershomu, mwana wa Mose, akawa kuhani wao. Wazawa wake pia walikuwa makuhani wa kabila la Dani mpaka wananchi wa nchi hiyo walipopelekwa uhamishoni. Wakati wote nyumba ya Mungu ilipokuwa huko Shilo, watu wa kabila la Dani waliiabudu sanamu ya kuchonga ambayo Mika aliitengeneza. Wakati huo ambapo hapakuwepo na mfalme katika Israeli, kulikuwa na Mlawi fulani aliyeishi kama mgeni mbali katika eneo la milima ya Efraimu. Mtu huyo alichukua suria kutoka Bethlehemu nchini Yuda. Lakini suria huyo akamkasirikia; huyo Mlawi, akamwacha na kurudi nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu, akakaa kwa muda wa miezi minne. Siku moja, mumewe alikwenda kumtafuta; alikusudia kuongea naye vizuri na kumrudisha nyumbani kwake. Basi huyo mwanamume alikwenda pamoja na mtumishi wake na punda wawili. Basi yule mwanamke akampeleka ndani kwa baba yake, naye baba mkwe wake alipomwona akampokea kwa furaha. Baba mkwe wake akamkaribisha, naye akakaa huko kwa muda wa siku tatu; huyo Mlawi na mtumishi wake wakala, wakanywa na kulala huko. Siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, wakajitayarisha kuondoka; lakini baba wa yule mwanamke akamwambia, “Kwanza kula chakula kidogo upate nguvu, kisha uondoke.” Basi hao watu wawili wakakaa, wakala na kunywa pamoja. Kisha baba mkwe wake akamwambia, “Tafadhali ulale hapa usiku huu na kufurahi.” Yule mtu aliposimama akitaka kuondoka, baba mkwe wake akamhimiza abaki, naye akabaki. Siku ya tano huyo mtu aliamka asubuhi, akitaka kuondoka. Lakini baba yake yule mwanamke akamwambia, “Kwanza upate nguvu kwa kula, ungoje alasiri, halafu uondoke.” Basi wote wawili wakala pamoja. Huyo Mlawi na suria wake pamoja na mtumishi wake walipoinuka kwenda zao, baba mkwe wake akamwambia huyo Mlawi, “Sasa mchana umekwisha na jioni imekaribia. Ulale hapa, na kufurahi. Kesho asubuhi utaamka mapema kuanza safari yako ya kurudi nyumbani.” Lakini huyo mtu alikataa kulala huko usiku huo. Basi, akainuka, akaondoka akafika karibu na mji wa Yebusi (yaani Yerusalemu). Alikuwa na wale punda wake wawili waliotandikwa tayari, pamoja na suria wake. Walipokuwa wamekaribia mjini Yebusi, siku ilikuwa karibu imekwisha; naye mtumishi akamwambia bwana wake, “Sasa heri tuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo usiku huu.” Bwana wake akamjibu, “Hatutageuka na kuingia katika mji wa wageni ambao si Waisraeli. Tutaendelea na safari mpaka Gibea. Twende tukaribie sehemu hizo na kulala huko Gibea au Rama.” Basi, wakaendelea na safari yao mpaka jua likatua wakiwa karibu na mji wa Gibea ambao ni mji wa kabila la Benyamini. Wakaingia mjini wapate kulala humo usiku. Walipoingia mjini wakaenda kukaa kwenye uwanja wa wazi wa mji, kwani hakuna mtu aliyewakaribisha nyumbani kwake. Walipokuwa huko mzee mmoja akafika kutoka shambani kwake. Mzee huyo alikuwa mwenyeji wa nchi ya milima ya Efraimu na alikuwa akiishi huko Gibea kama mgeni. Wakazi wa mji wa Gibea walikuwa wa kabila la Benyamini. Mzee huyo alipotazama na kumwona huyo msafiri akiwa huko uwanjani, alimwuliza, “Umetoka wapi na unakwenda wapi?” Naye akamjibu, “Tumetoka Bethlehemu nchini Yuda na tunaelekea sehemu za mbali za eneo la milima ya Efraimu. Huko ndiko ninakoishi na sasa ninarudi safarini huko Bethlehemu katika Yuda na kurejea nyumbani; hakuna mtu hapa aliyetukaribisha nyumbani kwake. Lakini sisi watumishi wako tuna nyasi na malisho kwa ajili ya punda wetu. Pia nina mkate na divai; hivyo vinanitosha mimi, suria wangu na mtumishi wangu. Hatupungukiwi kitu chochote.” Huyo mzee akamwambia, “Amani iwe nanyi! Nitawapa mahitaji yote. Ila msilale huku uwanjani.” Hivyo akawapeleka nyumbani kwake na kuwapa punda wao malisho. Hao wasafiri wakanawa miguu yao, wakala na kunywa. Walipokuwa wanajifurahisha, kumbe wanaume mabaradhuli wa mji huo wakaja wakaizingira hiyo nyumba na kugonga mlangoni. Wakamwambia mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mwanamume aliyekuja kwako, tulale naye.” Lakini huyo mzee mwenye nyumba akatoka nje, akawaambia “Sivyo ndugu zangu; nawasihi msitende uovu huo. Huyu ni mgeni wangu, hivyo msimtendee ubaya huo. Ninaye bado binti yangu ambaye ni bikira na yupo pia yule suria wa mgeni wangu. Niruhusuni niwatoe nje, muwachukue na kuwatendea kama mnavyotamani; lakini mtu huyu msimtendee jambo hilo la kipumbavu.” Lakini wanaume hao hawakumsikiliza. Kwa hiyo Mlawi yule akamchukua suria wake na kumtoa kwao huko nje. Nao wakamchukua na kumnajisi usiku kucha mpaka asubuhi. Karibu na mapambazuko, wakamwacha aende zake. Asubuhi, yule mwanamke akaja mpaka mlangoni mwa nyumba alimokuwa bwana wake, akaanguka chini hapo mlangoni na kukaa hapo mpaka kulipopambazuka kabisa. Bwana wa mwanamke huyo alipoamka asubuhi, alifungua milango ya nyumba, akatoka nje ili aendelee na safari. Ghafla akamkuta suria wake amelala chini mlangoni, mikono yake ikishika kizingiti cha mlango. Akamwambia, “Simama twende.” Lakini yeye hakujibu kitu. Akamchukua, akamweka juu ya punda wake na kumpeleka mpaka nyumbani kwake. Alipofika nyumbani kwake akachukua kisu na kumkatakata yule suria vipande kumi na viwili. Kisha akavipeleka vipande hivyo katika maeneo yote ya nchi ya Israeli. Wale wote walioona jambo hilo wakasema, “Jambo kama hili halijawahi kutukia wala kuonekana tangu siku ile Waisraeli walipotoka nchini Misri mpaka leo. Tulifikirie, tushauriane na kuamua.” Watu wote wa Israeli, kutoka Dani hadi Beer-sheba, pamoja na watu wa nchi ya Gileadi, jumuiya nzima, walikusanyika huko Mizpa, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Viongozi wote wa makabila ya Israeli wakajitokeza mbele ya mkusanyiko wa watu wa Mungu. Wote, jumla walikuwa askari wa miguu wenye silaha 400,000. Nao watu wa kabila la Benyamini, wakapata habari kwamba watu wale wengine wa Israeli walikuwa wamekusanyika huko Mizpa. Basi Waisraeli wakamwuliza yule mwanamume Mlawi “Tueleze, uovu huo ulifanyikaje?” Yule Mlawi, mume wa yule suria, akawajibu, “Mimi na suria wangu tulifika mjini Gibea, mji wa kabila la Benyamini ili tulale huko usiku. Lakini watu wa mji wa Gibea wakaja usiku wakaizingira nyumba nilimokuwa nimelala. Walitaka kuniua, wakambaka suria wangu mpaka akafa. Mimi nikachukua maiti yake, nikamkatakata vipandevipande na kuvipeleka kwa makabila yote ya Israeli, maana wamefanya jambo la kuchukiza na potovu katika Israeli. Sasa enyi Waisraeli, shaurianeni na toeni uamuzi wenu.” Watu wote kwa pamoja, wakasimama na kusema, “Hakuna yeyote kati yetu atakayerudi hemani kwake au nyumbani kwake. Hivi ndivyo tutakavyofanya kuhusu Gibea: Tutapiga kura namna ya kuwashambulia. Tutachagua watu kumi katika kila watu mia moja wa Israeli, watu mia moja katika kila watu elfu moja, watu elfu moja katika kila watu elfu kumi. Hao watakuwa na jukumu la kuwaletea chakula wenzao watakaokuwa na kazi ya kuuadhibu mji wa Gibea katika nchi ya Benyamini kwa uhalifu wao na upotovu walioufanya katika Israeli.” Hivyo wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa moyo mmoja dhidi ya mji wa Gibea. Watu wa makabila ya Israeli wakatuma wajumbe mpaka kila sehemu ya kabila la Benyamini, wakisema, “Je, ni uovu gani huu uliotukia miongoni mwenu? Sasa tupeni hao watu mabaradhuli wa Gibea ili tuwaue na kutokomeza uovu huu kutoka Israeli.” Lakini watu wa kabila la Benyamini hawakuwasikiliza ndugu zao, Waisraeli. Basi walikusanyika huko Gibea kutoka katika kila mji wao, ili kupigana na Waisraeli. Watu wa kabila la Benyamini walikusanya kutoka miji yao jeshi la watu 26,000 wenye kutumia silaha, nao wakazi wa mji wa Gibea wakakusanya watu 700 waliochaguliwa. Kati ya watu hao waliochaguliwa kulikuwa na watu 700 waliotumia mkono wa kushoto; kila mmoja aliweza kurusha jiwe kwa kombeo na kulenga unywele bila kukosea. Waisraeli, licha ya wa kabila la Benyamini, walikusanya watu 400,000 wawezao kutumia silaha. Wote walikuwa hodari wa vita. Waisraeli wakaenda Betheli kutaka shauri kwa Mungu, wapate kujua kabila ambalo litakwenda kwanza kupigana na watu wa kabila la Benyamini. Mwenyezi-Mungu alitaja kabila la Yuda liende kwanza. Basi, Waisraeli wakaenda asubuhi, wakapiga kambi yao karibu na mji wa Gibea. Waisraeli wakatoka kupigana na watu wa kabila la Benyamini karibu na Gibea. Watu wa kabila la Benyamini wakatoka nje ya mji wa Gibea wakapigana na Waisraeli, wakawaangusha chini siku hiyo, watu wa Israeli 22,000. Lakini Waisraeli wakajipa moyo, wakajipanga tena kwa vita mahali pale walipojipanga kwa mara ya kwanza. Basi Waisraeli wakaenda juu, wakamlilia Mwenyezi-Mungu mpaka jioni. Kisha wakaomba shauri kwa Mwenyezi-Mungu: “Je, twende tena kupigana na ndugu zetu, wa kabila la Benyamini?” Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Nendeni mkapigane nao.” Hivyo siku ya pili Waisraeli wakakaribia kupigana na watu wa kabila la Benyamini. Siku hiyo ya pili watu wa kabila la Benyamini walitoka Gibea na kuwashambulia Waisraeli, wakawaangusha chini Waisraeli 18,000. Watu wote wa jeshi la Waisraeli wakaenda Betheli. Walikaa huko mbele ya Mwenyezi-Mungu wakiomboleza na kufunga mpaka jioni. Wakamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Waisraeli wakamwomba Mwenyezi-Mungu awape shauri. Wakati huo sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilikuwa huko Betheli. Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Aroni alikuwa na wajibu wa kuhudumu mbele yake. Waisraeli wakamwuliza Mwenyezi-Mungu, “Je, twende tena kupigana na ndugu zetu, watu wa kabila la Benyamini?” Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Nendeni. Kesho nitawatia mikononi mwenu.” Hivyo, Waisraeli wakaweka watu mafichoni kuuzunguka mji wa Gibea. Waisraeli wakaenda kupigana na watu wa kabila la Benyamini katika siku ya tatu. Wakajipanga dhidi ya mji wa Gibea kama walivyofanya nyakati za hapo awali. Kisha watu wa kabila la Benyamini walipotoka mjini kuanza kupigana na Waisraeli, walivutwa kutoka nje ya mji. Ilitokea tena kama walivyofanya nyakati za hapo awali wakawaua baadhi ya watu wa Israeli kwenye njia kuu zielekeazo miji ya Betheli na Gibea, mpaka mbugani. Waliua Waisraeli wapatao thelathini. Watu wa Benyamini wakafikiri, “Tumewapiga kama nyakati zilizopita.” Lakini Waisraeli wakasema, “Sisi tukimbie ili tuwavute mbali na mji hadi kwenye njia kuu.” Hivyo watu wote wa Israeli wakatoka kwenye sehemu yao na kujipanga tena huko Baal-tamari. Wenzao waliokuwa wanaotea wakatoka haraka mahali pao upande wa magharibi wa mji wa Gibea. Askari hodari waliochaguliwa kutoka makabila yote ya Israeli wakawasili hapo mbele ya mji wa Gibea. Vita vya siku hiyo vilikuwa vikali. Lakini watu wa Benyamini hawakufahamu kwamba kuangamia kwao kulikuwa karibu. Mwenyezi-Mungu aliwashinda watu wa Benyamini mbele ya Waisraeli. Waisraeli wakawaua watu wa Benyamini 25,100. Hao wote waliouawa walikuwa askari walioweza kutumia silaha. Hivyo watu wa kabila la Benyamini wakaona kwamba wameshindwa. Waisraeli walirudi nyuma kana kwamba wanawakimbia watu wa kabila la Benyamini, kwani walitegemea wenzao waliokuwa wamewekwa kuotea mji wa Gibea. Wale waliowekwa kuuotea mji walitoka haraka na kuushambulia mji wa Gibea na kuwaua wote waliokuwamo kwa upanga. Walikuwa wamekubaliana na wale watu wengine wa Israeli juu ya ishara moja. Walikubaliana kwamba wale waliokuwa wanaotea watakapoona moshi mkubwa unapanda juu kutoka mjini, basi, waushambulie mji. Wakati huo, watu wa kabila la Benyamini walikuwa tayari wameua watu wapatao thelathini wa Israeli na kuambiana, “Tumewapiga kama hapo awali.” Lakini ile ishara ya mnara wa moshi ilipoanza kutokea katika mji, watu wa kabila la Benyamini walipotazama nyuma yao, wakashangaa kuona kwamba mji wao ulikuwa unateketezwa moto. Ndipo Waisraeli wakageuka, na watu wa kabila la Benyamini wakakumbwa na fadhaa kwani sasa waliona kuwa kuangamia kwao kulikuwa kumekaribia. Kwa hiyo wakageuka, wakawakimbia Waisraeli kuelekea jangwani, lakini vita vikawakumba; wakajikuta wako katikati ya majeshi mawili ya Israeli, na askari waliotoka wakawaangamiza. Waisraeli waliwazingira watu wa kabila la Benyamini, wakawafuatia kutoka Noha hadi mashariki ya mji wa Gibea wakiwaua wengi wao. Siku hiyo watu 18,000 wa kabila la Benyamini, wote askari hodari, waliuawa. Watu wengine wa kabila la Benyamini waligeuka, wakakimbia kuelekea jangwani hadi mwamba wa Rimoni. Wengine 5,000 waliuawa kwenye njia kuu walipokuwa wanakimbia. Waisraeli waliendelea kuwafuatia vikali watu wa kabila la Benyamini hadi mji wa Gidomu wakawaua watu 2,000. Jumla ya watu wote wa kabila la Benyamini waliouawa siku hiyo ilikuwa 25,000, askari hodari wa kutumia silaha. Lakini wanaume 600 wa kabila la Benyamini walifaulu kukimbilia jangwani hadi kwenye mwamba wa Rimoni, wakakaa huko kwa muda wa miezi minne. Waisraeli wakawageukia watu wengine wa kabila la Benyamini, wakawaua wote: Wanaume, wanawake, watoto na wanyama. Na miji yote waliyoikuta huko wakaiteketeza moto. Waisraeli walikuwa wameapa huko Mizpa kwamba hakuna hata mmoja wao ambaye angemwachia binti yake aolewe kwa watu wa kabila la Benyamini. Basi, wakaenda mpaka Betheli wakakaa huko mbele ya Mungu hadi jioni. Wakapaza sauti na kulia kwa uchungu mwingi. Wakasema “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa nini jambo hili limetukia hata tupungukiwe na kabila katika Israeli?” Kesho yake watu waliamka mapema, wakajenga madhabahu, wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha wakaulizana, “Je, miongoni mwa makabila yote ya Israeli kuna kikundi chochote ambacho hakikuhudhuria mkutano uliofanyika mbele ya Mwenyezi-Mungu?” Walikuwa wamefanya kiapo kwamba mtu yeyote ambaye hatahudhuria mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa ni lazima auawe. Lakini Waisraeli wakawaonea huruma ndugu zao wa kabila la Benyamini, wakasema, “Leo kabila moja la Israeli limeangamia. Sasa tutafanya nini ili kuwapatia wake hao wanaume wa kabila la Benyamini waliosalia? Maana tulikwisha apa kwa jina la Mwenyezi-Mungu kuwa hatutawapa binti zetu wawe wake zao!” Wakataka kujua kama kulikuwa na kikundi chochote cha makabila ya Israeli ambacho hakikuhudhuria mkutano mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa. Wakagundua kwamba hakuna mtu yeyote kutoka Yabesh-gileadi aliyekuja kwenye mkutano huo. Waisraeli walipohesabiwa huko Mizpa hakuna mkazi yeyote wa Yabesh-gileadi aliyehudhuria. Hivyo jumuiya ya Israeli ikapeleka watu wake 12,000 walio hodari kabisa na kuwaamuru: “Nendeni mkawaue wakazi wa Yabesh-gileadi; wanawake pamoja na watoto. Mtawaua wanaume wote na wanawake wote wasio mabikira.” Basi wakakuta miongoni mwa wakazi wa Yabesh-gileadi wasichana 400 ambao hawakuwa wamelala na mwanamume yeyote, wakawapeleka kambini huko Shilo katika nchi ya Kanaani. Kisha jumuiya nzima ikawapelekea ujumbe wa amani watu wa kabila la Benyamini ambao walikuwa kwenye mwamba wa Rimoni. Wanaume hao wa kabila la Benyamini wakawarudia hao wenzao wakati huohuo. Basi wakapewa wale wanawake ambao walikuwa wamesalimishwa huko Yabesh-gileadi. Lakini wanawake hao hawakuwatosha. Waisraeli wakawaonea huruma watu wa kabila la Benyamini, maana Mwenyezi-Mungu alisababisha kuweko na mwanya katika Israeli. Kisha wazee wa jumuiya nzima wakasema, “Sasa tutafanya nini ili kuwapatia wanawake hao wanaume waliosalia kwa vile wanawake wote wa kabila la Benyamini waliangamia? Lazima wanaume waliosalia wa kabila la Benyamini wapewe wanawake ili waendeleze kabila, na hivyo kusipotee kabila lolote katika Israeli. Lakini hatuwezi kuwatoa binti zetu wawe wake zao, maana tulikwisha apa kwamba mtu yeyote atakayemwoza binti yake kwa mwanamume wa kabila la Benyamini alaaniwe.” Basi wakakumbuka kwamba sikukuu ya Mwenyezi-Mungu iliyofanyika kila mwaka huko Shilo, mji ulio kaskazini ya Betheli, kwenye njia kuu itokayo Betheli kwenda Shekemu, ilikuwa inakaribia. Kwa hiyo wakawaamuru wale wanaume wa kabila la Benyamini, “Nendeni mkavizie na kuotea katika mashamba ya mizabibu.” Muwe macho. Wasichana wa Shilo watakapotoka nje kucheza wakati wa sikukuu, tokeni kwenye mizabibu na kila mtu ajinyakulie msichana mmoja awe mkewe. Kisha mrudi katika nchi ya Benyamini. Baba zao au kaka zao wakija kutulalamikia tutawaambia, “Sisi tunawaombeni mwahurumie watu wa Benyamini na kuwaachia wawachukue hao wanawake; maana hatukuwapata katika vita vya Yabesh-gileadi. Na kwa vile nyinyi wenyewe hamkutupatia hao binti zenu, hamtahukumiwa.” Wale wanaume wa kabila la Benyamini wakafanya hivyo, kila mmoja akajichagulia msichana miongoni mwa wasichana waliotoka nje kucheza huko Shilo na kumchukua kuwa mkewe. Kisha wakarudi katika eneo lao, wakaijenga miji yao upya na kuishi humo. Wakati huohuo Waisraeli wakaondoka, kila mtu akarudi katika eneo la kabila lake na jamaa yake. Kila mtu alirudi katika sehemu aliyogawiwa. Siku hizo hapakuwepo na mfalme katika Israeli. Kila mtu alifanya kama alivyoona kuwa sawa. Hapo zamani, wakati waamuzi walipokuwa wanatawala Israeli, palitokea njaa nchini humo. Mtu mmoja kutoka Bethlehemu katika Yuda pamoja na mkewe na watoto wao wa kiume wawili walikwenda kuishi kwa muda nchini Moabu ili kuishi kama wageni. Mtu huyo aliitwa Elimeleki na mkewe aliitwa Naomi. Watoto wao wawili wa kiume, mmoja aliitwa Mahloni na mwingine Kilioni. Mtu huyo na jamaa yake walikuwa Waefrathi wa huko Bethlehemu katika Yuda. Walikwenda nchini Moabu, wakakaa huko. Lakini Elimeleki, mumewe Naomi, alifariki na Naomi akaachwa na wanawe wawili. Vijana hao walioa wasichana wa Kimoabu, Orpa na Ruthu. Baada ya miaka kumi hivi, Mahloni na Kilioni nao pia walifariki. Baadaye, Naomi alipata habari kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa amewabariki watu wake kwa kuwapa chakula. Basi, akaondoka kutoka Moabu kurudi kwao pamoja na wakwe zake. Akaondoka mahali pale alipoishi pamoja na wakwe zake, wakashika njia ya kurudi Yuda. Naye Naomi akawaambia hao wakwe zake wawili, “Rudini kila mmoja nyumbani kwa mama yake. Naomba Mwenyezi-Mungu awe mwema kwenu kama mlivyokuwa wema kwangu na kwa wale watu wangu waliofariki. Mwenyezi-Mungu awajalie, kila mmoja wenu apate mume na nyumba yake.” Kisha Naomi akawaaga kwa kuwabusu. Lakini wao walianza kulia kwa sauti na kumwambia, “La hasha! Tutakwenda pamoja nawe kwa watu wako.” Naye Naomi akawasihi, “Rudini, binti zangu. Kwa nini kunifuata? Je, mnafikiri naweza kupata tena watoto watakaokuwa waume zenu? Rudini nyumbani kwenu binti zangu, kwa maana mimi ni mzee mno, siwezi kuolewa tena. Hata kama ningesema ninalo tumaini, na hata kama ningepata mume usiku huu na kupata watoto, je, mngeweza kungoja mpaka wakue? Je, mngeweza kujizuia msiolewe na waume wengine? Sivyo, binti zangu! Mambo yangu ni magumu mno kwa ajili yenu, maana Mwenyezi-Mungu amenipiga kipigo.” Hapo walipaza sauti wakaanza kulia tena. Ndipo Orpa akamkumbatia mkwewe, akamuaga na kurudi nyumbani; lakini Ruthu, akaandamana naye. Basi Naomi akamwambia, “Ruthu, tazama dada yako amerudi nyumbani kwake na kwa mungu wake; basi, nawe pia urudi, umfuate dada yako.” Lakini Ruthu akamjibu, “Usinisihi nikuache wewe, wala usinizuie kufuatana nawe. Kokote utakakokwenda ndiko nami nitakakokwenda, na ukaapo nitakaa, watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapofia hapo nitakufa nami, na papo hapo nitazikwa; Mwenyezi-Mungu anipe adhabu kali kama nikitenganishwa nawe isipokuwa tu kwa kifo.” Naomi alipoona kuwa Ruthu ameamua kwenda pamoja naye, aliacha kumshawishi. Ndipo wote wawili wakaendelea na safari hadi Bethlehemu. Walipofika huko, watu wote walishangaa, hata wanawake wakaulizana, “Je, huyu ni Naomi?” Naomi akasema, “Msiniite tena Naomi niiteni Mara, kwa maana Mungu mwenye nguvu ameyafanya maisha yangu yawe machungu mno. Nilipoondoka hapa, nilikuwa na vitu vingi, lakini sasa Mwenyezi-Mungu amenirudisha mikono mitupu. Mbona mwaniita Naomi na hali Mwenyezi-Mungu ameniadhibu, naye Mungu Mwenye Nguvu amenitesa.” Hivyo ndivyo Naomi pamoja na Ruthu Mmoabu, mkwewe, walivyorejea kutoka Moabu, na kuwasili Bethlehemu wakati uvunaji wa shayiri ulipokuwa unaanza. Naomi alikuwa na ndugu aliyeitwa Boazi, wa ukoo wa Elimeleki mumewe. Huyo alikuwa mtu mashuhuri na tajiri. Siku moja, Ruthu Mmoabu alimwambia Naomi, “Niruhusu niende shambani kukusanya masalio ya mavuno. Nina hakika kumpata mtu ambaye ataniruhusu niokote nyuma yake.” Naomi akamwambia, “Haya, nenda binti yangu.” Basi Ruthu akaenda shambani, akawafuata wavunaji huku anayaokota masuke waliyoyaacha. Na kumbe akajikuta katika shamba la Boazi, yule wa ukoo wake Elimeleki. Baada ya muda, Boazi alifika kutoka Bethlehemu akawasalimu wavunaji, akasema, “Mwenyezi-Mungu awe nanyi.” Nao wakamjibu, “Mwenyezi-Mungu na akubariki.” Kisha Boazi akamwuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule msichana ni nani?” Huyo kiongozi wa wavunaji akajibu, “Ni msichana Mmoabu aliyekuja pamoja na Naomi kutoka katika nchi ya Moabu. Aliniomba nimruhusu awafuate nyuma wavunaji huku akiokota masazo kati ya miganda. Basi alikuja na amefanya kazi tangu asubuhi na ni sasa tu amekwenda kupumzika kibandani.” Ndipo Boazi akamwambia Ruthu, “Hebu sikiliza binti yangu. Usiende kuokota masuke mahali pengine ila katika shamba hili tu. Fuatana na wanawake hawa; angalia mahali wavunapo ujiunge nao. Nimewaonya vijana hawa wasikusumbue. Na ukiona kiu, nenda kwenye mitungi na unywe maji waliyoyateka hao vijana.” Hapo Ruthu akamwinamia Boazi mpaka chini kwa unyenyekevu, akamwambia, “Nimepataje kibali chako? Mbona unanihurumia na hali mimi ni mgeni tu?” Lakini Boazi akamjibu, “Nimeyasikia yote uliyomfanyia mama mkwe wako tangu mumeo afariki. Ninajua jinsi ulivyowaacha wazazi wako, ukaiacha nchi yako, na jinsi ulivyokuja kuishi kati ya watu ambao hukuwajua hapo awali. Mwenyezi-Mungu akujaze kwa yote uliyoyafanya. Mwenyezi-Mungu wa Israeli uliyemkimbilia akulinde chini ya mabawa yake, akupe thawabu kamilifu.” Ruthu akamjibu, “Bwana, wewe umenifanyia wema mkubwa sana. Ingawa mimi si kama mmoja wa watumishi wako, nimeridhika kwa kuwa umenifariji sana na kuongea nami kwa ukarimu.” Wakati wa chakula, Boazi alimkaribisha Ruthu akamwambia, “Karibu hapa, njoo ule mkate pia na uuchovye ndani ya divai.” Kwa hiyo Ruthu akaketi pamoja na wavunaji, na Boazi akampa nafaka iliyokaangwa, akala akashiba hata akabakiza. Na ikawa Ruthu alipoendelea kuokota mavuno, Boazi aliwaambia wafanyakazi wake, “Mwacheni akusanye hata mahali miganda ilipo wala msimkemee. Zaidi ya hapo, vuteni masuke kutoka katika matita na mumwachie aokote bila kumkaripia.” Basi Ruthu aliendelea kuokota masuke mpaka jioni; na baada ya kupura hiyo shayiri alipata debe moja na zaidi. Kisha akachukua mavuno hayo hadi mjini na kumwonesha mama mkwe wake kiasi alichookota. Pia alikitoa kile chakula alichobakiza baada ya kushiba, akampa. Basi mkwewe akamwuliza, “Uliokota wapi haya yote? Je, ulikuwa katika shamba la nani? Heri huyo aliyekufadhili.” Hapo Ruthu akamwambia Naomi kwamba alikuwa amefanya kazi katika shamba la mtu aliyeitwa Boazi. Basi, Naomi akamwambia mkwewe, “Mwenyezi-Mungu ambariki Boazi! Mungu hutimiza daima ahadi zake kwa walio hai na waliokufa.” Kisha akaendelea kusema, “Huyo mtu ni ndugu yetu wa karibu na ni mmoja wa wale wenye wajibu wa kututunza.” Kisha Ruthu Mmoabu akasema, “Isitoshe, aliniambia nijiunge pamoja na wafanyakazi wake mpaka wamalize mavuno yote.” Basi, Naomi akamwambia Ruthu, “Naam binti yangu. Ni vyema kufanya kazi pamoja na wanawake wengine katika shamba la Boazi, kwa maana labda ungesumbuliwa kama ungekwenda katika shamba la mtu mwingine.” Kwa hiyo, Ruthu akafanya kazi nao, akaokota masuke mpaka mavuno ya ngano na shayiri yalipomalizika. Wakati huo wote alikuwa anakaa na mama mkwe wake. Baada ya muda, Naomi mkwewe alimwambia Ruthu, “Ni wajibu wangu kukutafutia mume ili upate mema. Sasa huyu Boazi, ambaye ulifanya kazi na wasichana wake, je, si ni wa ukoo wetu? Haya basi sikiliza, jioni hii atakuwa anapura shayiri. Kwa hiyo, nawa, ujipake manukato na kuvalia vizuri, kisha uende mahali anapopuria; lakini angalia usitambulike kwake mpaka atakapomaliza kula na kunywa. Pia, ujue mahali atakapolala, na akisha kusinzia, mwendee polepole uifunue miguu yake ulale papo hapo. Yeye atakueleza la kufanya.” Ruthu akajibu, “Nitafanya yote uliyoniambia.” Kwa hiyo, Ruthu alikwenda mahali pa kupuria, akafanya jinsi mama mkwe wake alivyomwamuru. Boazi alipomaliza kula na kunywa, akafurahi moyoni. Basi alikwenda karibu na tita la shayiri, akalala. Ruthu alikwenda polepole akafunua miguu yake na kulala hapo. Usiku wa manane, Boazi aligutuka, akageuka, akashtuka kumkuta mwanamke amelala miguuni pake. Akauliza, “Wewe ni nani?” Ruthu akajibu, “Ni mimi Ruthu, mtumishi wako. Kwa kuwa wewe u jamaa yangu wa karibu, uitande nguo yako juu ya mjakazi wako.” Boazi akasema, “Mwenyezi-Mungu na akubariki, kwa maana kwa yote unayofanya unaonesha heshima zaidi kuliko uliyoyafanya hapo awali, kwa maana hukuwatafuta vijana maskini au tajiri wakuoe. Sasa binti yangu usifadhaike, nitakufanyia lolote utakaloomba kwa kuwa kila mtu mjini humu anajua wema wako. Ni kweli kwamba ni jukumu langu kukutunza, lakini kuna pia mwenye jukumu la kukutunza na ambaye yu karibu zaidi kuliko mimi. Kwa hiyo, kaa hapa usiku wote, na kesho asubuhi tutaona kama atakubali kukutunza au la. Ikiwa atakutunza ni vyema. Akikataa, kwa jina la Mwenyezi-Mungu aliye hai mimi nitakutunza. Lala hapa mpaka asubuhi.” Basi Ruthu akalala hapo miguuni pake mpaka asubuhi, lakini aliamka alfajiri ili asionekane, kwa kuwa Boazi hakutaka mtu ajue kuwa Ruthu alikuwa mahali pa kupuria. Boazi akamwambia, “Tandika nguo yako chini.” Ruthu akafanya hivyo. Boazi akamwaga shayiri ipatayo vipimo sita, akamtwika, naye akarudi mjini. Alipofika mjini, mkwewe akamwuliza, “Ilikuwaje binti yangu?” Ruthu akamweleza yote ambayo Boazi alimtendea. Halafu akaendelea kusema, “Aliniambia nisirudi nyumbani kwa mkwe wangu mikono mitupu na kwa hiyo alinipa shayiri hii ipatayo vipimo sita.” Naye Naomi akasema, “Sasa tulia binti yangu Ruthu, mpaka uone litakalotokea. Boazi hatatulia leo mpaka ameyatimiza yote.” Boazi alikwenda mahali pa kufanyia mkutano huko kwenye lango la mji akaketi chini. Kisha yule ndugu ya Elimeleki ambaye Boazi alikuwa amemtaja, akapita karibu na hapo. Boazi akamwita, akasema, “Njoo, uketi hapa ndugu.” Basi huyo mtu akaja na kuketi hapo. Ndipo Boazi akawaita wazee kumi wa mji, akawaomba wao pia waketi hapo. Wakaketi. Ndipo Boazi akamwambia yule ndugu yake, “Sasa Naomi ambaye amerudi kutoka Moabu, anataka kuliuza shamba ambalo lilikuwa la jamaa yetu Elimeleki. Basi mimi nimeona afadhali nikujulishe habari hii. Sasa ikiwa unalitaka shamba hili, toa fidia ulichukue mbele ya wazee wa watu wangu. Ikiwa unalitaka au hulitaki sema basi kwa kuwa nafasi ya kwanza ya kulifidia ni yako na yangu ni ya pili.” Naye akasema, “Mimi nitalifidia.” Boazi akasema, “Ni vyema, lakini ukilichukua hilo shamba kutoka kwa Naomi, basi utakuwa unamchukua pia Ruthu Mmoabu, mjane ambaye ni jamaa ya marehemu ili kwamba shamba hilo libaki katika jamaa ya huyo marehemu.” Yule jamaa aliyekuwa wa karibu akajibu, “Ikiwa ni hivyo, sitalifidia shamba hilo, kwa sababu yaonekana kuwa nitauharibu urithi wangu. Afadhali haki yangu ya kulichukua nikupe wewe, maana mimi siwezi kulifidia.” Siku zile, katika Israeli ikiwa watu walitaka kukomboa au kubadilishana kitu, ilikuwa ni desturi kwa mtu kuonesha ishara kwa kuvua kiatu chake na kumpa mwingine. Kwa ishara hiyo Waisraeli walionesha kwamba mambo yamesawazishwa. Basi, mtu huyo alimwambia Boazi, “Lifidie shamba,” kisha alivua kiatu chake na kumpa. Ndipo Boazi akawaambia wazee na watu waliokuwa hapo, “Leo nyinyi ni mashahidi wangu. Mmeona kwamba nimenunua kutoka kwa Naomi, vyote vilivyokuwa vya Elimeleki, na vya Kilioni na Mahloni. Zaidi ya hayo, Ruthu Mmoabu mjane wa Mahloni, nimemnunua ili awe mke wangu. Mapatano haya yatafanya mali ya jamaa ya marehemu na ukoo wake kubakia kwa watu wake katika mji huu. Nyinyi ni mashahidi.” Basi wazee waliokuwa langoni na watu wote waliokuwapo walijibu, “Ndiyo, sisi ni mashahidi. Mwenyezi-Mungu amfanye mke wako awe kama Raheli na Lea, ambao wote wawili waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe upate kustawi katika jamaa ya Efratha, uwe na sifa katika Bethlehemu. Kwa sababu ya watoto Mwenyezi-Mungu atakaokupatia ambao mwanamke huyu atakuzalia, nayo nyumba yako iwe kama nyumba ya Peresi ambaye Tamari alimzalia Yuda.” Kwa hiyo, Boazi akamchukua Ruthu akawa mke wake. Mwenyezi-Mungu alimjalia Ruthu naye akachukua mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Ndipo wanawake wa mji huo wakamwambia Naomi, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye hakukuacha leo bila kuwa na jamaa aliye karibu wa kukutunza; naye awe mwenye sifa kubwa katika Israeli. Yeye atakurudishia uhai wako na atakutunza katika uzee wako; maana mkwe wako anayekupenda ambaye ana thamani kubwa zaidi kwako kuliko watoto wa kiume saba, ndiye amemzaa.” Basi Naomi alimchukua mtoto huyo akamweka kifuani mwake na kumlea. Wanawake majirani walimwita mtoto huyo Obedi wakisema, “Mtoto amezaliwa kwa Naomi.” Hatimaye Obedi akamzaa Yese aliyemzaa Daudi. Na hivi ndivyo vizazi vya Peresi: Peresi alimzaa Hesroni, Hesroni akamzaa Rami, Rami akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nahshoni, Nahshoni akamzaa Salmoni, Salmoni akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obedi, Obedi akamzaa Yese na Yese akamzaa Daudi. Kulikuwa na mtu mmoja mjini Rama katika nchi ya milima ya Efraimu aitwaye Elkana wa kabila la Efraimu. Yeye alikuwa mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu. Elkana alikuwa na wake wawili, mmoja aliitwa Hana na wa pili Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Kila mwaka Elkana alisafiri kutoka Rama kwenda kuabudu na kumtambikia Mwenyezi-Mungu wa majeshi kule Shilo. Huko, watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu. Kila wakati Elkana alipotoa tambiko alimpa mkewe Penina fungu moja la nyama ya tambiko na fungu mojamoja kwa watoto wake wa kiume na wa kike. Lakini Elkana alimpa Hana fungu moja ingawa alikuwa anampenda sana, na Mwenyezi-Mungu hakuwa amemjalia watoto. Lakini Penina, mchokozi wa Hana, daima alikuwa akimkasirisha vikali na kumuudhi Hana kwa kuwa Mwenyezi-Mungu hakumjalia watoto. Mambo haya yaliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Penina alimkasirisha Hana hata ikawa Hana analia na kukataa kula chochote. Elkana, mumewe, kila mara alimwuliza, “Kwa nini unalia? Kwa nini hutaki kula? Kwa nini una huzuni moyoni mwako? Je, mimi si bora kwako kuliko watoto kumi wa kiume?” Siku moja, walipokuwa wamemaliza kula na kunywa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, Hana akasimama. Wakati huo, kuhani Eli alikuwa amekaa kwenye kiti karibu na mwimo wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hana alikuwa na huzuni sana. Na alipokuwa anamwomba Mwenyezi-Mungu akawa analia kwa uchungu. Akaweka nadhiri akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kama tu utayaangalia mateso yangu mimi mtumishi wako ukanikumbuka mimi, bila kunisahau, mimi mtumishi wako, ukanijalia mimi mtumishi wako, mtoto wa kiume, nitakupa wewe Mwenyezi-Mungu mtoto huyo awe wako maisha yake yote; wembe hautapita kichwani pake kamwe.” Hana aliendelea kumwomba Mwenyezi-Mungu kwa muda mrefu, na kuhani Eli akawa anaangalia midomo yake. Hana alikuwa akiomba kimoyomoyo, lakini midomo yake ilikuwa inachezacheza, ila sauti yake haikusikika. Hivyo Eli akafikiri kuwa Hana amelewa. Kwa hiyo Eli akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achana na kunywa divai.” Lakini Hana akamjibu, “Sivyo bwana wangu; mimi ni mwanamke mwenye taabu mno; mimi sijanywa divai wala kinywaji kikali, bali nimekuwa nikimtolea Mwenyezi-Mungu yaliyomo rohoni mwangu. Usinidhanie kuwa mimi ni mwanamke asiyefaa kitu. Kwa muda wote huu nimekuwa nikisema mahangaiko yangu na taabu yangu.” Ndipo Eli akamwambia, “Nenda kwa amani; naye Mungu wa Israeli akupe kile ulichomwomba.” Hana akasema, “Naomba nami mtumishi wako nipate kibali mbele yako.” Hana akaenda zake, akala chakula na hakuwa na huzuni tena. Kesho yake asubuhi, Elkana na jamaa yake waliamka asubuhi na mapema, na baada ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu, walirudi nyumbani Rama. Elkana akalala na mkewe Hana, naye Mwenyezi-Mungu akamkumbuka. Hivyo Hana akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Hana akamwita mtoto huyo Samueli, kwani alisema, “Nimemwomba kwa Mwenyezi-Mungu.” Elkana na jamaa yake yote wakaenda tena Shilo na kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko ya kila mwaka na kutimiza nadhiri. Lakini safari hii Hana hakwenda, kwani alimwambia hivi mumewe, “Mara mtoto atakapoachishwa kunyonya, nitampeleka ili awekwe mbele ya Mwenyezi-Mungu, abaki huko daima.” Elkana, mumewe, akamjibu, “Fanya unaloona linafaa. Ngojea hadi utakapomwachisha mtoto kunyonya. Mwenyezi-Mungu aifanye nadhiri yako kuwa kweli.” Basi, Hana alibaki nyumbani, akaendelea kumlea mtoto wake hadi alipomwachisha kunyonya. Alipomwachisha kunyonya alimpeleka pamoja na fahali wa miaka mitatu, gunia la unga na kiriba cha divai. Hana alimwingiza mtoto kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, naye mtoto alikuwa mdogo tu. Walipokwisha kumchinja yule fahali, walimpeleka mtoto kwa kuhani Eli. Hana akamwambia, “Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyekuwa anasimama mbele yako akimwomba Mwenyezi-Mungu. Nilimwomba anipe mtoto huyu, na yeye alinipa kile nilichomwomba. Kwa sababu hiyo, mimi ninampa Mwenyezi-Mungu mtoto huyu; wakati wote atakapokuwa hai, ametolewa kwa Mwenyezi-Mungu.” Halafu, wakamwabudu Mwenyezi-Mungu hapo. Halafu Hana aliomba na kusema: “Namshangilia Mwenyezi-Mungu moyoni mwangu. Namtukuza Mwenyezi-Mungu aliye nguvu yangu. Nawacheka adui zangu; maana naufurahia ushindi wangu. “Hakuna aliye mtakatifu kama Mwenyezi-Mungu; hakuna yeyote aliye kama yeye; hakuna aliye mwamba kama Mungu wetu. Acheni kujisifu, acheni kusema ufidhuli. Maana ajuaye ni Mwenyezi-Mungu. Yeye huyapima matendo yote. Pinde za wenye nguvu zimevunjika. Lakini wadhaifu wanaendelea kupata nguvu. Wale ambao zamani walikuwa na chakula tele, sasa wanaajiriwa ili wapate chakula. Lakini waliokuwa na njaa, sasa hawana njaa tena. Mwanamke tasa amejifungua watoto saba. Lakini mama mwenye watoto wengi, sasa ameachwa bila mtoto. Mwenyezi-Mungu huua na hufufua; yeye huwashusha chini kuzimu naye huwarudisha tena. Mwenyezi-Mungu huwafanya baadhi wawe maskini, na baadhi wawe matajiri. Wengine huwashusha, na wengine huwakweza. Huwainua maskini toka mavumbini; huwanyanyua wahitaji toka majivuni, akawaketisha pamoja na wakuu, na kuwarithisha viti vya heshima. Maana, minara ya dunia ni ya Mwenyezi-Mungu; yeye ameisimika dunia juu ya minara yake. “Maisha ya waaminifu wake huyalinda, lakini maisha ya waovu huyakatilia mbali gizani. Maana, binadamu hapati ushindi kwa nguvu zake. Maadui wa Mwenyezi-Mungu watavunjwa vipandevipande; atanguruma dhidi yao kama radi mbinguni. Mwenyezi-Mungu ataihukumu dunia yote; atampa nguvu mfalme wake ataukuza uwezo wa mteule wake.” Kisha, Elkana akarudi nyumbani Rama. Lakini mtoto Samueli akabaki Shilo kumtumikia Mwenyezi-Mungu chini ya uongozi wa kuhani Eli. Watoto wa kiume wa Eli walikuwa walaghai sana. Hawakumjali Mwenyezi-Mungu wala juu ya vitu ambavyo watu walipaswa kuwapa makuhani. Kila mara mtu alipokuwa anatolea tambiko yake, mtumishi wa kuhani alikuja na uma wenye meno matatu; na wakati nyama ikiwa bado inachemka, huyo mtumishi aliuchomeka uma huo ndani ya chungu, nyama yoyote iliyotolewa humo na uma huo, ilikuwa mali ya kuhani. Waisraeli wote waliokwenda Shilo kutolea tambiko zao walitendewa hivyo. Zaidi ya hayo, hata kabla mafuta hayajachomwa, mtumishi wa kuhani huja na kumwambia yule mtu anayetoa tambiko, “Mtolee kuhani nyama ya kubanika maana yeye hatapokea nyama yako iliyochemshwa, bali iliyo mbichi.” Na kama mtu huyo akimjibu, “Ngojea kwanza nichome mafuta halafu utachukua kiasi chochote unachotaka,” hapo huyo mtumishi wa kuhani humjibu, “La, ni lazima unipe sasa hivi. La sivyo, nitaichukua kwa nguvu.” Dhambi hii ya vijana hao wa Eli ilikuwa kubwa sana mbele ya Mwenyezi-Mungu. Maana, vijana hao walidharau matoleo ya Mwenyezi-Mungu. Wakati huo, kijana Samueli aliendelea kumtumikia Mwenyezi-Mungu, akiwa amevaa kizibao cha kitani. Kila mwaka mama yake alimfumia vazi dogo, na kumpelekea alipokuwa akienda na mumewe kutolea tambiko ya kila mwaka. Eli aliwabariki Elkana na mkewe, akisema, “Mwenyezi-Mungu na akupe wewe Elkana watoto wengine kwa mwanamke huyu ili wachukue mahali pa yule uliyempa Mwenyezi-Mungu.” Kisha wao hurudi nyumbani. Mwenyezi-Mungu alimhurumia Hana naye akajaliwa kupata watoto wa kiume watatu na mabinti wawili. Mtoto Samueli akaendelea kukua mbele ya Mwenyezi-Mungu. Wakati huo Eli alikuwa mzee sana. Aliposikia yote ambayo watoto wake wa kiume walikuwa wanawatendea Waisraeli, jinsi walivyokuwa wanalala na wanawake waliokuwa wanahudumu kwenye mlango wa hema la mkutano, aliwauliza, “Kwa nini mnafanya mambo haya? Nasikia kutoka kwa watu wote juu ya maovu mnayoyafanya. Msifanye hivyo wanangu kwa sababu mambo hayo ninayoyasikia kutoka kwa watu wa Mwenyezi-Mungu ni mabaya. Mtu akimkosea mwenzake, anaweza kuombewa kwa Mungu, ili Mungu amsamehe. Lakini mtu akimkosea Mwenyezi-Mungu nani awezaye kumwombea msamaha?” Lakini watoto hao hawakumsikiliza baba yao, kwani Mwenyezi-Mungu alikwisha kata shauri kuwaua. Mtoto Samueli aliendelea kukua, akazidi kupendwa na Mwenyezi-Mungu na watu. Siku moja, mtu wa Mungu alimwendea Eli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Nilijijulisha kwa jamaa ya Aroni, wazee wako, walipokuwa watumwa wa Farao nchini Misri. Kati ya makabila yote ya Israeli nilimchagua Aroni na jamaa yake kuwa makuhani wangu, wanitumikie madhabahuni, wafukize ubani na kuvaa kizibao mbele yangu. Nikaipatia jamaa ya mzee wako tambiko zangu ambazo Waisraeli walinitolea kwa moto. Kwa nini basi, umezionea wivu tambiko na sadaka nilizowaamuru watu waniletee? Wewe umewastahi watoto wako kuliko mimi kwa kujinenepesha nyinyi wenyewe kwa kula sehemu nzurinzuri za sadaka ambazo watu wangu wa Israeli hunitolea!’ Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anatamka hivi, ‘Niliahidi kwamba jamaa yako na jamaa ya wazee wako mtakuja mbele yangu kunitumikia milele;’ lakini sasa Mwenyezi-Mungu anakutangazia hivi, ‘Jambo hilo liwe mbali nami.’ Nitawaheshimu wale wanaoniheshimu, na wale wanaonidharau, nitawadharau. Angalia siku zaja ambapo nitawaua vijana wote wa kiume katika jamaa yako na katika ukoo wako, hata hakutakuwa na mwanamume yeyote atakayeishi awe mzee. Utakuwa na wasiwasi na utawaonea wenzio kijicho kwa zile baraka zote ambazo nitawapa watu wengine wa Israeli, lakini hakuna mtu katika jamaa yako atakayeishi na kuwa mzee. Mtu wako ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahu yangu atakuwa amenusurika ili nimpofushe macho yake, naye atakufa moyo na wazawa wako watauawa kikatili. Na litakalowapata watoto wako wawili wa kiume, Hofni na Finehasi, ni hili: Wote wawili watakufa siku moja. Hii itakuwa ni ishara kwako. Kisha, nitajiinulia kuhani mwingine mwaminifu atakayefanya kulingana na yale yaliyomo moyoni na akilini mwangu. Nitamjengea ukoo imara, naye atahudumu daima mbele ya mfalme wangu. Yeyote atakayebakia katika jamaa yako atamwendea kuhani huyo na kumwomba kipande cha fedha au mkate, na kumwambia, ‘Niweke, nakuomba, kwenye nafasi mojawapo ya kuhani ili niweze, angalau, kupata kipande cha mkate.’” Wakati huo, kijana Samueli alipokuwa anamtumikia Mwenyezi-Mungu chini ya uangalizi wa Eli, ujumbe kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ulikuwa haba sana; hata na maono kutoka kwake yalipatikana mara chache. Siku moja usiku, Eli ambaye macho yake yalikuwa yamefifia, alikuwa amelala katika chumba chake. Samueli naye alikuwa amelala ndani ya hekalu la Mwenyezi-Mungu karibu na sanduku la agano la Mungu. Taa ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa bado inawaka kwani kulikuwa hakujapambazuka. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwita Samueli! Naye Samueli, akaitika, “Naam!” Kisha Samueli akamwendea Eli kwa haraka, akamwambia, “Nimekuja kwani umeniita.” Lakini Eli akamwambia, “Mimi sijakuita. Nenda ukalale.” Samueli akarudi na kulala. Mwenyezi-Mungu akamwita tena, “Samueli!” Samueli akaamka, akamwendea Eli na kumwambia, “Nimekuja, kwani umeniita.” Lakini Eli akamwambia, “Sikukuita mwanangu, kalale tena.” Samueli alikuwa hamjui Mwenyezi-Mungu bado, wala ujumbe wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa bado haujafunuliwa kwake. Mwenyezi-Mungu akamwita Samueli kwa mara ya tatu. Samueli akaamka, akamwendea Eli na kumwambia, “Nimekuja, kwani umeniita.” Ndipo Eli alipotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyemwita Samueli. Kwa hiyo Eli akamwambia Samueli, “Nenda ukalale, na akikuita, mwambie hivi: ‘Sema, ee Mwenyezi-Mungu, kwani mimi mtumishi wako nasikiliza.’” Hivyo Samueli akarudi na kulala mahali pake. Baadaye Mwenyezi-Mungu akaja na kusimama hapo, akamwita Samueli kama hapo awali, “Samueli! Samueli!” Samueli akasema, “Sema, kwani mimi mtumishi wako nasikiliza.” Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Tazama, nataka kutenda jambo fulani katika Israeli ambalo kila atakayesikia, atashtuka kulisikia. Siku hiyo, nitatimiza yale yote niliyosema tangu mwanzo hadi mwisho dhidi ya Eli kuhusu jamaa yake. Nimekwisha mwambia kuwa nitaiadhibu jamaa yake milele, kwa uovu anaoujua kwa sababu watoto wake wa kiume wamenikufuru mimi na hakuwazuia. Kwa hiyo naapa kuhusu jamaa ya Eli kwamba uovu wao hautaondolewa kamwe kwa tambiko wala kwa sadaka.” Samueli akalala pale hadi asubuhi, kisha akaamka na kufungua milango ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Lakini Samueli aliogopa kumwambia Eli maono hayo. Hata hivyo, Eli alimwita Samueli, akamwambia, “Mwanangu Samueli.” Samueli akaitika, “Naam!” Eli akamwuliza, “Je, Mwenyezi-Mungu alikuambia nini? Usinifiche alichokuambia. Ikiwa utanificha alichokuambia, Mungu atakuadhibu vikali.” Basi, Samueli akamweleza Eli yote aliyoambiwa, bila kumficha chochote. Ndipo Eli akasema, “Yeye ni Mwenyezi-Mungu; na afanye anachoona ni chema kwake.” Samueli aliendelea kukua na Mwenyezi-Mungu akawa pamoja naye, na yale yote aliyosema hakuna hata moja ambalo halikutimia. Watu wote kote nchini Israeli toka Dani, upande wa kaskazini, hadi Beer-sheba, upande wa kusini, wakajua kuwa Samueli alikuwa nabii mwaminifu wa Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu alizidi kujionesha huko Shilo, ambako alimtokea Samueli na kuongea naye. Naye Samueli aliposema kitu, Waisraeli wote walimsikiliza. Wakati huo, Wafilisti walikutana pamoja, wapigane na Waisraeli. Waisraeli walipiga kambi yao huko Ebenezeri, na Wafilisti wakapiga kambi yao huko Afeka. Wafilisti waliwashambulia Waisraeli, na baada ya mapigano makali, Waisraeli walishindwa. Waisraeli 4,000 waliuawa kwenye uwanja wa mapambano. Wanajeshi walionusurika walipowasili kambini, wazee wa Israeli walisema, “Kwa nini Mwenyezi-Mungu amewaacha Wafilisti watushinde leo? Twendeni tukalilete sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu kutoka Shilo, ili aweze kwenda nasi vitani na kutuokoa kutoka na zetu.” Hivyo, walituma watumishi huko Shilo, nao wakalileta sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu wa majeshi ambaye anakaa kifalme juu ya viumbe wenye mabawa. Wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi walikuja pamoja na lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipofika kambini Waisraeli wote walishangilia kwa furaha, hata nchi yote ikatikisika. Wafilisti waliposikia sauti hiyo ya furaha walisema “Kelele hizo zote kambini mwa Waebrania zina maana gani?” Walipojua kwamba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilikuwa limewasili kambini mwa Waisraeli, Wafilisti waliogopa; wakasema, “Bila shaka, miungu imewasili kambini mwao! Ole wetu! Jambo kama hili halijawahi kutokea. Ole wetu! Ni nani atakayeweza kutuokoa kutokana na miungu hiyo yenye nguvu? Hiyo ni miungu iliyowaua Wamisri kwa kila aina ya mapigo jangwani. Sasa, enyi Wafilisti, jipeni moyo. Muwe, hodari msije mkawa watumwa wa Waebrania kama wao walivyokuwa watumwa wetu. Muwe hodari kama wanaume na kupigana.” Wafilisti walipiga vita, na Waisraeli walishindwa na kukimbia kila mtu nyumbani kwake. Siku hiyo kulikuwa na mauaji makubwa kwani askari wa miguu 30,000 wa Israeli waliuawa. Sanduku la agano la Mungu lilitekwa, na wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa. Siku hiyohiyo, mtu mmoja wa kabila la Benyamini alikimbia kutoka mstari wa mbele wa mapigano mpaka Shilo huku mavazi yake yakiwa yamechanika na akiwa na mavumbi kichwani. Eli, akiwa na wasiwasi moyoni kuhusu sanduku la Mungu, alikuwa ameketi kwenye kiti chake, kando ya barabara akiangalia. Yule mtu alipowasili mjini na kueleza habari hizo, mji mzima ulilia kwa sauti. Eli aliposikia sauti ya kilio, akauliza, “Kelele hizo ni za nini?” Yule mtu akaenda haraka kwa Eli ili kumpa habari hizo. Wakati huo, Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane na macho yake yalikuwa yamepofuka. Yule mtu akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi; nimekimbia kutoka vitani leo.” Eli akamwuliza, “Mwanangu, mambo yalikuwaje huko?” Yule aliyeleta habari akasema, “Waisraeli wamewakimbia Wafilisti. Kumekuwa na mauaji makubwa miongoni mwa Waisraeli. Zaidi ya yote, wanao wote wawili, Hofni na Finehasi, wameuawa, na sanduku la agano la Mungu limetekwa.” Huyo mtu alipotaja tu sanduku la Mungu, Eli alianguka chali kutoka kwenye kiti chake kando ya lango. Eli alipoanguka hivyo, shingo yake ilivunjika kwani alikuwa mzee na mnene, naye akafariki. Eli alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka arubaini. Tena ilitokea kwamba, mkwewe Eli, yaani mke wa Finehasi, wakati huo alikuwa mjamzito, na muda wake wa kujifungua ulikuwa umekaribia. Aliposikia kwamba sanduku la agano la Mungu limetekwa na kwamba baba mkwe wake, hata na mumewe wamefariki, mara moja alipata utungu, na kujifungua. Basi, alipokuwa anakufa, wanawake waliokuwa wanamsaidia walimwambia, “Usiogope, maana umejifungua mtoto wa kiume.” Lakini yeye hakujibu neno, wala hakuwasikiliza. Naye akamwita mtoto wake Ikabodi, akimaanisha, “Utukufu wa Mungu umeondoka Israeli,” akiwa na maana kwamba sanduku la agano lilikuwa limetekwa, tena baba mkwe wake na mumewe, wote walifariki. Akasema, “Utukufu wa Mungu umeondoka Israeli kwani sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu limetekwa.” Baada ya Wafilisti kuliteka sanduku la Mungu, walilibeba kutoka mji wa Ebenezeri hadi mji wao wa Ashdodi. Kisha, wakalipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu kwenye hekalu la mungu wao Dagoni na kuliweka karibu naye. Kesho yake asubuhi, watu wa mji wa Ashdodi walipoamka waliona sanamu ya Dagoni imeanguka kifudifudi mbele ya sanduku la Mungu. Wakaisimamisha tena sanamu ya Dagoni na kuiweka tena mahali pake. Lakini, kesho yake asubuhi walipoamka, waliona kuwa sanamu ya Dagoni imeanguka kifudifudi mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu, kichwa, miguu na mikono ya sanamu hiyo, vyote vilikuwa vimekatika, vikawa vimelala chini kwenye kizingiti cha mlango. Kiwiliwili cha sanamu ya Dagoni ndicho tu kilikuwa kimebakia. Ndio maana makuhani wa Dagoni na wote wanaoingia kumwabudu Dagoni huko Ashdodi, wanapoingia kwenye hekalu la Dagoni hawakanyagi kizingiti cha hekalu la Dagoni hadi leo. Mwenyezi-Mungu aliwaadhibu vikali na kuwatisha watu wa Ashdodi. Aliwaadhibu, hata na majirani zao, kwa kuwaletea ugonjwa wa majipu. Wakazi wa Ashdodi walipoyaona mambo yaliyowapata, wakasema, “Mungu wa Israeli anatuadhibu vikali sisi pamoja na mungu wetu Dagoni. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu haliwezi kukaa kwetu.” Walituma wajumbe na kuwakusanya wakuu wote wa Wafilisti na kuwauliza, “Je, tutafanya nini na sanduku hili la Mungu wa Israeli?” Wakuu wao wakajibu, “Sanduku hilo la Mungu wa Israeli lipelekeni Gathi.” Basi, wakalipeleka kwenye mji wa Gathi. Lakini baada ya kulipeleka huko Gathi, Mwenyezi-Mungu akauadhibu mji huo, akisababisha hofu kuu mjini, na akawapiga wanaume wa mji huo, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu. Hivyo, wakalipeleka sanduku hilo la Mungu kwenye mji wa Ekroni. Lakini sanduku hilo la Mungu lilipofika huko, watu wa mji huo walipiga kelele, “Wametuletea sanduku la Mungu wa Israeli ili kutuua sisi na watu wetu.” Kisha wakatuma ujumbe na kukusanya wakuu wa Wafilisti na kuwaambia, “Lirudisheni sanduku la Mungu wa Israeli mahali pake, ili lisituue sisi pamoja na watu wetu.” Walifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na hofu kubwa katika mji mzima kwa sababu Mungu alikuwa anawaadhibu vikali. Nao wale ambao hawakufa walipatwa na majipu hata kilio cha mji kilifika mbinguni. Baada ya sanduku la Mwenyezi-Mungu kukaa katika nchi ya Wafilisti kwa muda wa miezi saba, Wafilisti waliwaita makuhani na waaguzi wao na kuwauliza, “Tufanyeje na sanduku hili la Mwenyezi-Mungu? Tuambieni namna gani tunavyoweza kulirudisha mahali pake.” Wao wakawaambia, “Mkirudisha sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu. Lakini kwa vyovyote vile mnapolirudisha pelekeni na sadaka ya kuondoa hatia ili kuondoa hatia yenu. Mkifanya hivyo mtapona, nanyi mtafahamu kwa nini amekuwa akiwaadhibu mfululizo.” Watu wakauliza, “Tutampelekea sadaka gani ya kuondoa hatia?” Wao wakawajibu “Vinyago vitano vya dhahabu vilivyo mfano wa majipu, na vinyago vitano vya dhahabu vikiwa mfano wa panya, kila kimoja kikiwakilisha mkuu mmoja wa Wafilisti, kwani tauni iliyotumwa kwenu ni ileile iliyotumwa kwa wakuu wenu. Lazima mfanye vinyago vya majipu na vinyago vya panya wenu, vitu ambavyo vinaangamiza nchi yenu. Ni lazima mumpe heshima Mungu wa Israeli. Labda ataacha kuwaadhibu, nyinyi wenyewe, miungu yenu na nchi yenu. Kwa nini mnakuwa wakaidi kama Wamisri na Farao? Je, Mungu alipowadhihaki Wamisri, hawakuwaacha Waisraeli waondoke, nao wakaondoka? Basi, tayarisheni gari jipya na ng'ombe wawili wakamuliwao ambao bado hawajafungwa nira; wafungeni kwenye gari hilo lakini ndama wao wasiende pamoja nao, ila wabaki zizini. Chukueni sanduku la Mwenyezi-Mungu na kuliweka katika gari hilo. Kando ya sanduku wekeni vile vinyago vya dhahabu ambavyo mnampelekea kama sadaka ya kuondoa hatia yenu. Kisha mliache liende litakakokwenda. Bali angalieni, ikiwa gari hilo linakwenda moja kwa moja kuelekea nchi yake yaani kwenye mji wa Beth-shemeshi, basi, hapo tutajua kuwa aliyetuletea tauni hii ni Mungu wa Israeli. Lakini kama haliendi huko, basi, tutajua kuwa sio mkono wake uliotupiga, bali maafa haya yametupata kwa bahati mbaya.” Walifanya kama walivyoambiwa; waliwachukua ng'ombe wawili wanaokamuliwa na kuwafunga kwenye gari, na ndama wao wakawafunga zizini. Lile sanduku la Mwenyezi-Mungu wakalitia kwenye gari hilo pamoja na lile kasha lenye vinyago vya dhahabu vya panya na vile vya majipu. Hao ng'ombe walikwenda moja kwa moja kuelekea mji wa Beth-shemeshi bila kupinda kushoto au kulia, na walikuwa wanalia walipokuwa wanakwenda. Wale wafalme watano wa Wafilisti waliwafuata hadi mpakani mwa Beth-shemeshi. Watu wa Beth-shemeshi walikuwa wanavuna ngano bondeni. Walipotazama juu na kuliona sanduku la Mwenyezi-Mungu, wakafurahi sana. Hilo gari lilielekea kwenye shamba la Yoshua, mkazi wa Beth-shemeshi. Lilipofika hapo likasimama karibu na jiwe kubwa. Watu wakalibomoa lile gari, wakatumia mbao zake kwa kuwateketeza hao ng'ombe ambao waliwatoa kama sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi-Mungu. Walawi walikuwa wameliteremsha sanduku la Mwenyezi-Mungu na lile kasha lenye vinyago vya dhahabu na kuviweka kwenye lile jiwe kubwa. Basi, siku hiyo watu wa Beth-shemeshi walitoa sadaka za kuteketezwa, na kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Wale wakuu watano wa Wafilisti walipoona hayo, walirudi Ekroni, siku hiyohiyo. Wafilisti walivipeleka vile vinyago vitano vya dhahabu na vya majipu kwa Mwenyezi-Mungu vikiwa sadaka ya kuondoa hatia yao, kinyago kimoja kwa ajili ya mji mmoja: Mji wa Ashdodi, mji wa Gaza, mji wa Ashkeloni, mji wa Gathi na kwa mji wa Ekroni. Walipeleka pia vinyago vitano vya dhahabu vya panya kulingana na hesabu ya miji yote ya Wafilisti iliyotawaliwa na wakuu watano wa Wafilisti. Miji hiyo ilikuwa yenye ngome na vijiji ambavyo havikuzungushiwa kuta. Lile jiwe kubwa kwenye shamba la Yoshua wa Beth-shemeshi, mahali ambapo walilipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu, ni ushahidi wa tukio hilo hadi leo. Mwenyezi-Mungu aliwaua wakazi sabini wa mji wa Beth-shemeshi, kwa sababu waliangalia ndani ya sanduku lake. Watu waliomboleza kwa sababu Mwenyezi-Mungu alikuwa amefanya mauaji makubwa miongoni mwao. Kisha, wakazi wa mji wa Beth-shemeshi wakasema: “Nani awezaye kusimama mbele ya Mwenyezi-Mungu, huyu Mungu mtakatifu? Atakwenda kwa nani ili aondoke kwetu?” Walituma wajumbe kwenda kwa wakazi wa mji wa Kiriath-yearimu, waseme: “Wafilisti wamelirudisha sanduku la Mwenyezi-Mungu, njoni mlichukue.” Kisha, watu wa Kiriath-yearimu wakaenda na kulichukua sanduku la Mwenyezi-Mungu, wakalipeleka nyumbani kwa Abinadabu, aliyeishi milimani. Wakamweka wakfu mtoto wake wa kiume aliyeitwa Eleazari ili alitunze sanduku hilo. Tangu sanduku la Mwenyezi-Mungu lipelekwe mjini Kiriath-yearimu muda mrefu ulipita, miaka ishirini hivi. Wakati huo Waisraeli wote walimlilia Mwenyezi-Mungu. Samueli akawaambia Waisraeli, “Kama mnamrudia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wenu wote, ni lazima mwondoe kati yenu miungu ya kigeni na sanamu za Ashtarothi. Mwelekeeni Mwenyezi-Mungu kwa moyo wote, na kumtumikia yeye peke yake; naye atawaokoa kutoka mikononi mwa Wafilisti.” Hivyo, Waisraeli wakatupilia mbali sanamu za Mabaali na Maashtarothi, wakamtumikia Mwenyezi-Mungu peke yake. Kisha, Samueli akawaita Waisraeli wote wakutane huko Mizpa, akawaambia, “Huko nitamwomba Mwenyezi-Mungu kwa ajili yenu.” Hivyo, Waisraeli wote wakakusanyika huko Mizpa. Walichota maji na kuyamimina mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakafunga siku ile yote na kusema, “Tumetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu.” (Samueli alikuwa mwamuzi wa Waisraeli huko Mizpa). Wafilisti waliposikia kuwa Waisraeli wamekusanyika huko Mizpa, wakuu watano wa Wafilisti wakaenda kuwashambulia. Waisraeli waliposikia juu ya jambo hilo waliwaogopa Wafilisti. Basi, wakamwambia Samueli, “Usiache kumlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa ajili yetu. Endelea kumlilia atuokoe kutoka kwa Wafilisti.” Kwa hiyo Samueli alichukua mwanakondoo anayenyonya akamtolea Mwenyezi-Mungu kama sadaka ya kuteketezwa nzima. Kisha Samueli akamlilia Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya Israeli, naye akajibu kilio chake. Samueli alipokuwa anatoa ile sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti walikaribia kuwashambulia Waisraeli. Lakini Mwenyezi-Mungu akatoa sauti kubwa ya ngurumo dhidi ya Wafilisti, na kuwavuruga Wafilisti, nao wakatimuliwa mbele ya Waisraeli. Waisraeli walitoka Mizpa na kuwafuatilia Wafilisti mpaka karibu na mji wa Beth-kari, wakawaangamiza. Kisha, Samueli alichukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mizpa na Sheni, akaliita jiwe hilo Ebenezeri akisema, “Mwenyezi-Mungu ametusaidia mpaka sasa.” Siku hiyo Wafilisti walishindwa; na Mwenyezi-Mungu aliwazuia Wafilisti kuivamia nchi ya Israeli wakati wote Samueli alipokuwa hai. Miji yote ya Waisraeli ambayo Wafilisti waliiteka kati ya Ekroni na Gathi ilirudishiwa Waisraeli, nao walikomboa nchi yao kutoka kwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Waisraeli na Waamori. Samueli alikuwa mwamuzi wa Israeli maisha yake yote. Kila mwaka Samueli alitembelea Betheli, Gilgali na Mizpa, na kuwaamua Waisraeli katika miji hiyo yote. Kisha, alikuwa akirudi Rama, maana huko kulikuwa nyumbani kwake; aliwaamulia Waisraeli haki zao huko, na kumjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu huko. Samueli alipokuwa mzee, aliwafanya watoto wake wa kiume kuwa waamuzi wa Israeli. Mtoto wake wa kwanza wa kiume aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya. Wote wawili walikuwa waamuzi huko Beer-sheba. Lakini watoto hao hawakufuata mwenendo wa baba yao. Bali walianza kujitafutia faida. Wakapokea rushwa na kupotosha haki. Basi, viongozi wote wa Israeli walikusanyika pamoja, na kumwendea Samueli mjini Rama, wakamwambia, “Tazama, wewe sasa ni mzee na watoto wako hawafuati mwenendo wako. Hivyo, tuteulie mfalme wa kututawala kama yalivyo mataifa mengine.” Lakini jambo la Waisraeli kutaka wapewe mfalme wa kuwatawala, halikumpendeza Samueli. Naye akamwomba Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sikiliza kila kitu ambacho watu wanakuambia; maana hawajakukataa wewe, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme juu yao. Tangu nilipowatoa Misri, wameniacha mimi, wamekuwa wakiitumikia miungu mingine mpaka leo. Sasa hayo matendo ambayo wamekuwa wakinitendea mimi, ndiyo wanayokutendea na wewe. Basi, wasikilize, lakini, waonye vikali, na waeleze waziwazi jinsi mfalme atakayewatawala atakavyowatendea.” Kwa hiyo, Samueli akawaambia wale watu waliokuwa wanaomba wapewe mfalme maneno yote ya Mwenyezi-Mungu. Samueli aliwaambia, “Hivi ndivyo mfalme wenu atakayewatawala atakavyowatendea: Watoto wenu wa kiume atawafanya wawe waendeshaji wa magari yake, na wengine kuwa wapandafarasi wake, na wengine watapiga mbio mbele ya magari yake. Atajichagulia wengine wawe makamanda wa vikosi vyake vya maelfu na wengine wawe makamanda wa vikosi vya watu hamsinihamsini. Atawafanya wengine wamlimie mashamba yake na kuvuna mazao yake. Atawafanya wengine pia wamtengenezee zana za vita, na wengine wamtengenezee vipuli vya magari yake. Binti zenu atawachukua kuwa watengenezaji marashi, wengine wapishi na wengine waokaji mikate. Atayachukua mashamba yenu mazuri, mashamba ya mizeituni, na mashamba ya mizabibu na kuwapa watumishi wake. Atachukua sehemu ya kumi ya nafaka zenu na ya zabibu zenu na kuwapa maofisa wake na watumishi wake. Atachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike na ng'ombe wenu wazuri na punda wenu wazuri kabisa na kuwafanya wamfanyie kazi zake. Atachukua sehemu ya kumi ya kondoo wenu. Na nyinyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. Wakati huo, nyinyi mtalalamika kwa sababu ya mfalme wenu ambaye mmejichagulia nyinyi wenyewe. Lakini Mwenyezi-Mungu hatawajibu.” Hata hivyo watu walikataa kumsikiliza Samueli, wakasema, “La! Sisi tutakuwa na mfalme juu yetu, ili nasi pia tuwe kama mataifa mengine. Mfalme wetu, atatuhukumu, atatuongoza na kutupigania vita vyetu.” Samueli alipokwisha sikiliza kila kitu walichosema, akaenda na kumweleza Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Wasikilize na wapatie mfalme.” Kisha Samueli akawaambia Waisraeli warudi nyumbani, kila mtu mjini kwake. Katika kabila la Benyamini, kulikuwa na mtu mmoja tajiri aliyeitwa Kishi. Yeye alikuwa mtoto wa Abieli, mwana wa Zero, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia Mbenyamini. Kishi alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Shauli. Shauli alikuwa kijana mzuri, na hakuna mtu katika Israeli aliyelingana na Shauli kwa uzuri. Shauli alikuwa mrefu zaidi kuliko mtu yeyote katika nchi ya Israeli; watu wote walimfikia mabegani. Siku moja, punda wa Kishi, baba yake Shauli, walipotea. Hivyo, Kishi akamwambia Shauli, “Mchukue mmoja wa watumishi, uende kuwatafuta punda.” Wakawatafuta kwenye nchi ya milima ya Efraimu na eneo la Shalisha, lakini hawakuwaona huko. Halafu wakafika Shalimu, na huko hawakuwaona. Wakawatafuta katika nchi ya Benyamini, hata hivyo hawakuwapata. Walipofika kwenye nchi ya Sufu, Shauli alimwambia mtumishi wake, “Turudi nyumbani, la sivyo baba yangu ataacha kufikiria juu ya punda, na badala yake atakuwa na wasiwasi juu yetu.” Yule mtumishi akamwambia, “Ngoja kidogo; katika mji huu kuna mtu wa Mungu ambaye anaheshimiwa sana; kila asemalo huwa kweli. Sasa tumwendee, labda anaweza kutuambia jinsi safari yetu itakavyokuwa.” Shauli akamwuliza, “Lakini tukimwendea, tutampa nini? Tazama, mikate katika mifuko yetu imekwisha na hatuna chochote cha kumpa huyo mtu wa Mungu. Tuna nini?” Yule mtumishi akamjibu Shauli, “Ona, mimi nina fedha robo shekeli. Nitampa huyo mtu wa Mungu ili atuambie juu ya safari yetu.” (Hapo awali katika Israeli kama mtu akitaka kumwomba Mungu shauri, alisema, “Haya, njoo, twende kwa mwonaji.” Kwani mtu anayeitwa nabii siku hizi hapo awali aliitwa mwonaji). Shauli akamjibu, “Hilo ni jambo jema; haya, twende.” Hivyo, wakaenda kwenye mji alimokuwa anakaa yule mtu wa Mungu. Walipokuwa wanapanda mlima kuelekea mjini, wakakutana na wasichana waliokuwa wakienda kuteka maji. Wakawauliza wasichana hao, “Je, mwonaji yuko mjini?” Wale wasichana wakawajibu, “Ndiyo, yuko. Tena yuko mbele yenu; mkifanya haraka mtamkuta. Ameingia tu mjini leo, kwa sababu leo watu watatambika huko mlimani. Mara mtakapoingia mjini, mtamkuta kabla hajaenda mahali pa ibada mlimani ili kula. Maana watu hawatakula mpaka kwanza yeye abariki tambiko. Baadaye wale walioalikwa watakula. Hivyo nendeni haraka; mtakutana naye mara.” Hivyo Shauli na mtumishi wake walikwenda mjini. Walipokuwa wanaingia mjini, walimwona Samueli akitoka mjini, na anaelekea mahali pa juu. Jana yake, kabla Shauli hajafika mjini hapo, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia hivi Samueli: “Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya kabila la Benyamini, nawe utampaka mafuta kuwa mtawala wa watu wangu Israeli. Yeye atawaokoa watu wangu kutoka kwa Wafilisti, kwani nimeyaona mateso ya watu wangu na kilio chao kimenifikia.” Samueli alipomwona tu Shauli, Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Huyu ndiye yule mtu niliyekuambia. Yeye ndiye atakayewatawala watu wangu.” Hapo Shauli alimwendea Samueli aliyekuwa karibu na lango la mji na kumwuliza, “Nakuomba unioneshe nyumba ya mwonaji.” Samueli akamjibu; “Mimi ndiye mwonaji. Nitangulieni kwenda mahali pa juu kwani leo mtakula pamoja nami. Kesho asubuhi maswali yote uliyo nayo nitayajibu. Kuhusu wale punda waliopotea siku tatu zilizopita, msiwe na wasiwasi juu yao; wamekwisha patikana. Lakini ni nani yule ambaye Waisraeli wanamtaka sana? Je, si wewe na jamaa yote ya baba yako?” Shauli akajibu: “Mimi ni wa kabila la Benyamini, kabila dogo kuliko makabila yote ya Israeli. Na katika kabila lote la Benyamini jamaa yangu ndiyo ndogo kabisa. Lakini, kwa nini unanizungumzia namna hiyo?” Kisha Samueli akampeleka Shauli na mtumishi wake sebuleni, akawapa mahali pa heshima, ambako wageni walioalikwa walikuwa wamekaa. Kulikuwa na wageni wapatao thelathini. Samueli akamwambia mpishi, “Lete ile sehemu niliyokupatia, nikakuambia uiweke kando.” Yule mpishi akaenda akaleta paja na sehemu ya nyama iliyokuwa upande wa juu wa paja hilo na kuviweka mbele ya Shauli. Ndipo Samueli akamwambia Shauli, “Tazama kile ulichowekewa; sasa kimewekwa mbele yako. Sasa ule kwa sababu kimewekwa kwa ajili yako ili upate kula pamoja na wageni.” Hivyo, Shauli akala pamoja na Samueli siku hiyo. Waliporudi mjini kutoka mahali pa juu pa ibada, Shauli alitandikiwa kitanda kwenye paa la nyumba, akalala huko. Alfajiri na mapema, Samueli alimwita Shauli kutoka darini: “Amka, ili nikusindikize urudi nyumbani.” Shauli aliamka, na wote wawili, yeye na Samueli, wakatoka na kwenda barabarani. Walipofika mwisho wa mji, Samueli akamwambia Shauli, “Mwambie huyo kijana atangulie mbele yetu.” Kijana alipokwisha ondoka, Samueli akaendelea kusema, “Ngoja kidogo, nami nitakufunulia yale aliyosema Mungu.” Ndipo Samueli akachukua chupa ndogo ya mafuta akammiminia Shauli kichwani, akambusu na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu amekutia mafuta uwe mtawala juu ya watu wake. Leo tutakapoagana, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli huko Selsa katika nchi ya Benyamini. Hao watakuambia kuwa wale punda uliokuwa unawatafuta wamekwisha patikana. Baba yako ameacha kufikiri juu ya punda, ila ana wasiwasi juu yako, akijiuliza kila mara, ‘Nitafanya nini juu ya mwanangu?’ Kutoka hapo utakwenda kwenye mwaloni wa Tabori, mahali ambapo utakutana na wanaume watatu wakiwa njiani kwenda kumtolea Mungu tambiko, huko Betheli. Mmoja wao atakuwa anawachukua wanambuzi watatu, wa pili atakuwa anachukua mikate mitatu na wa tatu atakuwa amebeba kiriba cha divai. “Watakusalimia na kukupa mikate miwili, nawe utaipokea mikononi mwao. Kisha, utakapofika huko Gibea-elohimu, mahali ambapo pana kambi ya kijeshi ya Wafilisti; hapo, utakapokuwa unakaribia mji, utakutana na kundi la manabii. Manabii hao watakuwa wanatoka mahali pa juu huku wakipiga vinubi, matari, filimbi na zeze, na watakuwa wanatabiri. Roho ya Mwenyezi-Mungu itakujia kwa nguvu, nawe utaanza kutabiri pamoja nao na kugeuka kuwa mtu mwingine. Wakati mambo haya yatakapokutokea, chochote utakachoweza kufanya kifanye, kwani Mungu yu pamoja nawe. Utanitangulia kwenda mjini Gilgali, mahali ambapo nitakukuta na kutoa sadaka ya kuteketezwa na tambiko za amani. Utaningojea hapo kwa muda wa siku saba mpaka nije na kukuonesha la kufanya.” Shauli alipogeuka ili kumwacha Samueli, Mungu akabadili moyo wa Shauli. Yale yote aliyoambiwa na Samueli yakatokea siku hiyo. Shauli na mtumishi wake walipofika huko Gibea, alilakiwa na kundi la manabii. Roho ya Mungu ilimjia kwa nguvu, na Shauli akaanza kutabiri pamoja na manabii hao. Watu waliomfahamu Shauli hapo awali, walipomwona anatabiri, wakaulizana, “Kitu gani kimempata mwana wa Kishi? Je, hata Shauli ni mmoja wa manabii?” Mtu fulani, mkazi wa mahali hapo, akasema, “Je, baba yao ni nani?” Hivyo kukazuka methali isemayo, “Je, hata Shauli ni mmoja wa manabii?” Shauli alipomaliza kutabiri, alikwenda mahali pa ibada juu. Baba mdogo wa Shauli alipowaona Shauli na mtumishi, akawauliza, “Mlikuwa wapi?” Shauli akajibu, “Tulikwenda kuwatafuta punda, na tulipoona hawapatikani, tulikwenda kumwona Samueli.” Yule baba mdogo wa Shauli akamwambia, “Tafadhali, niambie kile alichokuambia Samueli.” Shauli akajibu, “Alituambia waziwazi kuwa punda wamepatikana.” Lakini Shauli hakumweleza kuwa Samueli alimwambia kuwa atakuwa mfalme. Samueli aliwaita watu wote wakusanyike mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa. Walipowasili aliwaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: Niliwatoa Waisraeli nchini Misri, nikawaokoa nyinyi kutoka kwa Wamisri na falme nyingine zilizowakandamiza. Lakini leo hii mmenikataa mimi Mungu wenu ambaye nawaokoa kutoka maafa na huzuni zenu; nanyi mmesema, ‘La! Tuwekee mfalme juu yetu.’ Sasa, basi, jikusanyeni nyote mbele yangu mkiwa katika makabila yenu na kwa maelfu yenu.” Kisha Samueli akayapanga makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachukuliwa kwa kura. Akalileta mbele kabila la Benyamini, kulingana na koo zake, na ukoo wa Matri ukachaguliwa kwa kura. Mwisho akauleta mbele ukoo wa Matri, na Shauli mwana wa Kishi akachaguliwa kwa kura. Lakini walipomtafuta hakupatikana. Wakamwuliza Mungu tena, “Je, kuna mtu zaidi anayekuja?” Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Anajificha kwenye mizigo.” Basi, walikwenda mbio, wakamtafuta Shauli na kumleta. Shauli aliposimama miongoni mwa watu alikuwa mrefu kuliko watu wote, kuanzia mabegani. Samueli akawaambia watu wote, “Huyu ndiye mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu katika watu wote; hakuna yeyote aliye kama yeye.” Watu wote wakapiga kelele: “Aishi mfalme.” Kisha, Samueli aliwaeleza watu juu ya wajibu na haki za mfalme, akaziandika katika kitabu ambacho alikiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kisha, Samueli aliwaaga watu wote, kila mtu aende nyumbani kwake. Pia, Shauli pamoja na wapiganaji hodari ambao awali Mungu aligusa mioyo yao, alikwenda nyumbani kwake huko mjini Gibea. Lakini watu wengine wasiofaa kitu, walisema, “Je, mtu huyu anaweza kutuokoa?” Walimdharau Shauli na hawakumpa zawadi yoyote. Lakini yeye hakukasirika. Kisha mfalme Nahashi wa Waamoni, alikwenda na kuuzingira mji wa Yabesh-gileadi. Wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi wakamwambia Nahashi, “Fanya mapatano nasi, nasi tutakutumikia.” Lakini akawaambia, “Nitafanya mapatano nanyi kwa sharti moja kwamba nitamngoa kila mmoja wenu jicho lake la kulia; hivyo nitawaaibisha Waisraeli wote.” Wazee wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe muda wa siku saba ili tuwatume wajumbe katika nchi yote ya Israeli. Kama hakuna mtu yeyote wa kutuokoa, tutajisalimisha wenyewe kwako.” Wale wajumbe walipofika mjini Gibea, alikoishi Shauli, wakaeleza habari hizo na watu wote wakaanza kulia kwa sauti. Sasa, Shauli alikuwa anatoka shambani akiwa na fahali wake, akauliza, “Watu wana nini? Kwa nini wanalia?” Wakamwambia habari waliyoleta wajumbe kutoka Yabeshi. Mara, Shauli aliposikia maneno hayo, roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, naye akawaka hasira kali. Akachukua fahali wawili akawakatakata vipandevipande, akatuma wajumbe wavipitishe kila mahali nchini Israeli wakisema, “Mtu yeyote ambaye hatamfuata Shauli na Samueli vitani, fahali wake watafanywa hivyo.” Hofu ikawaaingia Waisraeli kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu angeweza kufanya. Kwa hiyo, wote walitoka kwa pamoja. Shauli alipowapanga Waisraeli huko Bezeki akawa na watu 300,000 kutoka Israeli na 30,000 kutoka Yuda. Wakawaambia wale wajumbe waliorudi kutoka Yabeshi, “Waambieni hivi wakazi wa Yabesh-gileadi: Kesho, wakati jua linapokuwa kali, mtakuwa mmekombolewa.” Watu wa Yabeshi walipopata habari hizo walifurahi sana. Hivyo, wakamkejeli Nahashi wakimwambia, “Kesho tutajisalimisha kwako, nawe utatutendea lolote unaloona ni jema.” Kesho yake, Shauli aliwagawa watu katika vikosi vitatu. Wakati wa zamu ya asubuhi, wakaingia kwenye kambi ya adui, na kuwashambulia Waamoni. Kufikia adhuhuri adui wengi walikuwa wamekatiliwa mbali. Wale walionusurika walitawanyika ovyo, hata kusiwe kikundi chochote cha watu wawili pamoja. Ndipo Waisraeli wakamwambia Samueli, “Wako wapi wale watu waliosema Shauli asiwe mfalme juu yetu? Tuletee watu hao, nasi tutawaulia mbali.” Lakini Shauli akawaambia, “Hakuna mtu yeyote atakayeuawa leo, kwa kuwa katika siku hii, Mwenyezi-Mungu ameikomboa Israeli.” Samueli akawaambia, “Twendeni wote Gilgali na kwa mara nyingine tutamtangaza Shauli kuwa mfalme.” Watu wote wakaenda Gilgali, na walipofika huko, wakamtawaza Shauli kuwa mfalme mbele ya Mwenyezi-Mungu. Wakamtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za amani hapo. Na Shauli pamoja na watu wote wa Israeli wakafurahi sana. Samueli akawaambia Waisraeli wote, “Yote mliyoniambia, nimeyasikiliza. Nimemtawaza mfalme juu yenu. Sasa, mnaye mfalme wa kuwaongoza. Kwa upande wangu, mimi ni mzee mwenye mvi, na watoto wangu wa kiume wako pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu nilipokuwa kijana mpaka sasa. Niko hapa, na kama nimefanya tendo lolote lile baya, basi, toeni ushahidi mbele ya Mwenyezi-Mungu na mbele ya mfalme wake mteule. Je, nimepora fahali au punda wa mtu yeyote? Je, nimempunja mtu yeyote? Je, nimemkandamiza mtu yeyote? Je, nimepokea rushwa kwa mtu yeyote ili kupotosha haki? Nami nitamrudishia chochote kile.” Watu wakamjibu, “Kamwe hujatudanganya, hujatukandamiza, wala hujachukua kitu chochote kwa mtu.” Samueli akajibu, “Mwenyezi-Mungu ni shahidi juu yenu, na mfalme wake mteule leo ni shahidi kuwa mmeniona sina hatia.” Wao wakajibu: “Yeye ni shahidi.” Samueli akawaambia, “Mwenyezi-Mungu ndiye aliyemteua Mose na Aroni na kuwatoa babu zenu nchini Misri. Sasa simameni papo hapo mlipo ili mimi na nyinyi tuhukumiwe mbele ya Mwenyezi-Mungu, nami nitawahutubia kuhusu matendo yake ya ajabu ambayo aliyatenda ili kuwaokoa nyinyi na babu zenu. “Yakobo na jamaa yake walipokwenda Misri, na Wamisri walipowakandamiza, babu zenu walimlilia Mwenyezi-Mungu; naye akawatuma Mose na Aroni ambao waliwatoa babu zenu nchini Misri na kuwafanya mkae katika nchi hii. Lakini wao walimsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, naye akawatia mikononi mwa Sisera, kamanda wa jeshi la Hazori, na mikononi mwa Wafilisti na mikononi mwa mfalme wa Moabu. Mataifa hayo yalipigana na babu zenu na kuwashinda. Babu zenu wakamlilia Mwenyezi-Mungu, wakisema, ‘Tumefanya dhambi kwa sababu tumekuacha wewe Mwenyezi-Mungu, kwa kutumikia Mabaali na Maashtarothi. Tuokoe kutoka mikononi mwa adui zetu, nasi tutakutumikia’. Ndipo Mwenyezi-Mungu alipomtuma Yerubaali, na baadaye akamtuma Bedani, kisha Yeftha, na mwishowe akanituma mimi Samueli. Kila mmoja wetu aliwaokoa kutoka kwa adui zenu waliowazunguka, nanyi mkaishi kwa amani. Lakini mlipomwona mfalme Nahashi wa Waamoni amekuja kuwashambulia, mkamkataa Mwenyezi-Mungu ambaye ndiye Mfalme wenu, mkaniambia, ‘La! Mfalme ndiye atakayetutawala.’ Sasa, mfalme mliyejichagulia ndiye huyu hapa. Mlimwomba Mwenyezi-Mungu awape mfalme, naye amewapa. Kama mkimcha Mwenyezi-Mungu, na kumtumikia, na kusikiliza sauti yake bila kuiasi amri yake, kama nyinyi wenyewe pamoja na mfalme anayewatawala mkimfuata Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, basi mtafanikiwa. Lakini kama hamtasikiliza sauti ya Mwenyezi-Mungu, mkaasi amri yake, basi yeye atapambana nanyi pamoja na mfalme wenu. Kwa hiyo basi, tulieni na kulitazama jambo hilo kubwa ambalo Mwenyezi-Mungu atatenda mbele yenu. Je, sasa si wakati wa kuvuna ngano? Lakini mimi nitamwomba Mwenyezi-Mungu alete radi na mvua, nanyi mtatambua na kuona kuwa uovu wenu mliotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kujitakia mfalme, ni mkubwa.” Basi, Samueli akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akatuma radi na mvua katika siku hiyo. Watu wote wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu na Samueli. Hivyo wakamwambia Samueli, “Tafadhali utuombee sisi watumishi wako kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili tusife; kwa sababu tumezidisha dhambi zetu kwa uovu huo wa kujitakia mfalme.” Samueli akawajibu, “Msiogope; ingawa mmefanya uovu huu, msiache kumfuata Mwenyezi-Mungu, ila mtumikieni kwa moyo wenu wote. Msiifuate miungu ya uongo isiyo na faida wala haiwezi kuwaokoa, maana ni ya uongo. Kwa heshima ya jina lake kuu, Mwenyezi-Mungu hatawatupa watu wake kwa sababu amependa kuwafanya nyinyi muwe watu wake. Tena kwa upande wangu haitatokea niache kuwaombea kwa Mwenyezi-Mungu; kufanya hivyo itakuwa kumkosea Mwenyezi-Mungu. Nitaendelea kuwafundisha njia njema na ya haki. Basi, nyinyi mcheni Mwenyezi-Mungu na kumtumikia kwa uaminifu kwa moyo wenu wote. Kumbukeni yale mambo makuu aliyowatendea. Lakini kama mkiendelea kutenda maovu, mtaangamia nyinyi wenyewe pamoja na mfalme wenu.” Shauli alikuwa na umri wa miaka kadha wa kadha alipoanza kutawala. Na alitawala Israeli kwa muda wa miaka … miwili. Shauli aliwachagua Waisraeli 3,000. Kati yao, 2,000 alikuwa nao huko Mikmashi na katika nchi ya milima ya Betheli. Elfu moja aliwaweka huko Gibea katika eneo la Benyamini. Hao aliwaweka chini ya mwanawe Yonathani. Watu wengine wote waliobakia, aliwarudisha, kila mtu nyumbani kwake. Yonathani alishinda kambi ya kijeshi ya Wafilisti huko Geba, na Wafilisti wote walisikia juu ya habari hizo. Hivyo Shauli alipiga tarumbeta katika nchi yote akatangaza, akisema, “Waebrania na wasikie.” Waisraeli wote waliposikia kuwa Shauli alikuwa ameishinda ngome ya kijeshi ya Wafilisti, na kwamba Wafilisti wanawachukia sana Waisraeli, waliitwa kwenda kuungana na Shauli huko Gilgali. Wafilisti walikuwa na magari 30,000, askari 6,000 wapandafarasi na kikosi cha askari wa miguu wengi kama mchanga wa pwani; wote walipanda juu na kupiga kambi yao huko Mikmashi, mashariki ya Beth-aveni. Waisraeli walipoona wako taabuni (maana walikuwa wanashambuliwa vikali), walianza kujificha. Wengine walijificha mapangoni, wengine mashimoni, wengine kwenye miamba, wengine kwenye makaburi na wengine kwenye visima. Wengine walivuka mto Yordani mpaka katika nchi ya Gadi na nchi ya Gileadi. Lakini Shauli alikuwa bado huko Gilgali na watu wote walimfuata wakitetemeka. Shauli alimngoja Samueli kwa muda wa siku saba, kama Samueli alivyosema. Lakini Samueli hakuja huko Gilgali na watu walianza kumwacha Shauli. Basi, Shauli akawaambia watu, “Nileteeni sadaka yenu ya kuteketezwa na zile za amani.” Naye akatolea sadaka ya kuteketezwa. Mara tu alipokuwa anamaliza kutoa sadaka ya kuteketezwa, Samueli aliwasili. Shauli akatoka nje kwenda kumlaki Samueli na kumsalimia. Samueli akamwuliza, “Umefanya nini?” Shauli akamjibu, “Nilipoona watu wananiacha, na wewe hukuja, katika muda wa siku ulizosema, na tena nilipoona Wafilisti wamejipanga tayari kwa vita huko Mikmashi, nikawaza kwamba Wafilisti watakuja kunishambulia huko Gilgali. Tena nilikuwa bado sijaomba fadhili za Mwenyezi-Mungu. Ndipo nilipolazimika kutolea mimi mwenyewe sadaka ya kuteketezwa.” Samueli akamjibu Shauli, “Umefanya kipumbavu. Hukutii aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Kama ungetii, Mwenyezi-Mungu angeudumisha milele ufalme wako juu ya Israeli. Lakini sasa ufalme wako hautadumu kwa kuwa amri aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu hukuitii. Mwenyezi-Mungu amejitafutia mtu mwingine ambaye atamtii kwa moyo wote, na huyo ndiye ambaye amemteua kuwa mtawala juu ya watu wake.” Samueli akaondoka kutoka Gilgali na kwenda huko Gibea katika nchi ya Benyamini. Shauli alipowahesabu watu waliokuwa pamoja naye, aliona wako watu 600 tu. Shauli na Yonathani mwanawe pamoja na watu waliokuwa pamoja nao, walikaa huko Gibea katika nchi ya Benyamini na Wafilisti walipiga kambi huko Mikmashi. Wafilisti walitoka kwenye kambi yao kwenda kuwashambulia wakiwa wako katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra katika nchi ya Shuali. Kikosi kingine kilielekea Beth-horoni, na kikosi kingine kikageukia njia ielekeayo bonde la Seboimu, kuelekea jangwani. Wakati huo hapakuwepo na mhunzi yeyote katika nchi nzima ya Israeli, kwani Wafilisti walikusudia kuwazuia Waebrania wasije wakajitengenezea mapanga au mikuki. Kila Mwisraeli alilazimika kuwaendea Wafilisti kunoa wembe wa plau yake au sururu au shoka au mundu wa kuvunia. Waisraeli walikuwa wanalipa fedha theluthi mbili za shekeli kunoa wembe wa plau na sururu. Na bei ya kunoa shoka au kupata mchokoo ilikuwa theluthi moja ya shekeli. Kwa hiyo siku ya vita hakuna mtu miongoni mwa wote waliokuwa pamoja na Shauli na Yonathani aliyekuwa na upanga au mkuki isipokuwa Shauli na Yonathani mwanawe. Wafilisti walipeleka kikosi cha askari kwenda kulinda njia ya Mikmashi. Siku moja, Yonathani mwana wa mfalme Shauli alimwambia kijana aliyembebea silaha, “Njoo, twende ngambo kwenye ngome ya Wafilisti.” Lakini Yonathani hakumwambia baba yake. Shauli alikuwa amepiga kambi chini ya mkomamanga huko Migroni, nje ya mji wa Gibea, akiwa pamoja na watu wapatao 600. Ahiya, mwana wa Ahitubu ndugu yake Ikabodi mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Mwenyezi-Mungu mjini Shilo, alikuwa ndiye aliyevaa kizibao cha kuhani. Watu hawakujua kwamba Yonathani amekwisha ondoka. Kwenye kipito ambako Yonathani alipaswa apitie ili afike kwenye ngome ya Wafilisti, kulikuwa na miamba miwili iliyochongoka, upande huu na upande mwingine. Mwamba mmoja uliitwa Bosesi na mwingine uliitwa Sene. Mwamba mmoja ulikuwa kaskazini mwa mji wa Mikmashi na mwingine ulikuwa kusini mkabala na mji wa Gibea. Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha, “Njoo, twende upande wa pili kwenye ile ngome ya hawa watu wasiotahiriwa. Huenda Mwenyezi-Mungu akatusaidia, maana Mwenyezi-Mungu haokoi kwa kutegemea wingi au uchache wa watu.” Yule kijana aliyembebea silaha akamwambia, “Fanya chochote unachotaka kufanya, mimi niko pamoja nawe kwani wazo lako ndilo wazo langu.” Yonathani akamwambia, “Tutavuka kuwaendea wale watu ili wapate kutuona. Kama wakituambia tuwangoje, hadi waje hapa tulipo basi, tutasimama papa hapa na wala hatutawaendea. Lakini wakisema sisi tuwaendee, basi tutawaendea kwani hiyo itakuwa ni ishara kuwa Mwenyezi-Mungu amewatia mikononi mwetu.” Basi, wakajitokeza ili Wafilisti wawaone. Wafilisti walipowaona wakasema, “Angalieni wale Waebrania wanatoka kwenye mashimo walimokuwa wamejificha.” Wafilisti waliokuwa kwenye ngome wakamwita Yonathani na kijana aliyembebea silaha, “Njoni huku kwetu, nasi tutawaonesha kitu.” Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha, “Nifuate; Mwenyezi-Mungu amewatia mikononi mwa Israeli.” Basi, Yonathani akapanda kwa miguu na mikono, na yule kijana akamfuata. Yonathani aliwashambulia Wafilisti akiwaangusha chini huku yule kijana alifuata nyuma akiwaua. Katika mashambulizi hayo ya kwanza Yonathani, akiwa pamoja na kijana wake aliyembebea silaha, aliwaua watu kama ishirini katika eneo la nchi lipatalo nusu eka. Katika nchi nzima ya Wafilisti, wote walianza kufadhaika, wanajeshi kambini, watu mashambani, kwenye ngome, hata na washambuliaji walitetemeka; nchi ilitetemeka, na kulikuwa na woga mkubwa. Wapelelezi wa Shauli huko Gibea katika nchi ya Benyamini waliwaona watu wengi wakikimbia huku na huko. Shauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, “Hebu jihesabuni ili kujua ni akina nani waliotutoroka.” Walipojihesabu, waligundua kuwa Yonathani na kijana aliyembebea silaha walikuwa hawapo. Shauli akamwambia kuhani Ahiya, “Lilete hapa sanduku la Mungu.” (Wakati huo sanduku la agano la Mungu lilikuwa pamoja na Waisraeli.) Shauli alipokuwa anaongea bado na kuhani, ghasia kambini kwa Wafilisti ziliongezeka zaidi na zaidi. Kwa hiyo Shauli akamwambia kuhani, “Acha; usililete tena sanduku la agano.” Hivyo, Shauli na watu wake wakajipanga na kuingia vitani dhidi ya Wafilisti. Lakini Wafilisti walianza kushambuliana wenyewe kwa wenyewe kwa mvurugiko mkubwa. Waebrania waliokuwa upande wa Wafilisti, na waliokwenda nao huko kambini, wakageuka na kujiunga na Waisraeli waliokuwa pamoja na Shauli na Yonathani. Hata Waisraeli wengine waliokuwa wamejificha kwenye nchi ya milima ya Efraimu, waliposikia kuwa Wafilisti walikuwa wanakimbia, nao pia wakawafuatia na kuwapiga. Hivyo Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli ushindi. Vita vilienea mpaka kupita Beth-aveni. Siku ile, Waisraeli walisumbuliwa sana maana Shauli alikuwa amewaapisha watu, “Mtu yeyote atakayekula chakula kabla jua kutua, na kabla sijajilipiza kisasi cha adui zangu, na alaaniwe.” Hivyo, siku yote, hakuna mtu aliyeonja chakula chochote. Watu wote walipofika sehemu yenye msitu, walikuta asali kila mahali. Ingawa watu walipofika msituni na kukuta asali ikidondoka kila mahali hakuna mtu aliyethubutu kula asali hiyo kwa kuogopa kile kiapo walichoapishwa. Lakini Yonathani hakuwa amesikia baba yake alipowaapisha watu. Hivyo akainyosha fimbo aliyokuwa nayo, akaichovya kwenye sega la asali, akala asali hiyo. Hapo akajisikia kuwa na nguvu. Mtu mmoja akamwambia, “Baba yako aliwaapisha watu vikali, akisema, ‘Mtu yeyote atakayekula chakula leo na alaaniwe.’” Nao watu walikuwa hoi kwa njaa. Yonathani akajibu, “Baba yangu anawasumbua watu. Sasa mimi najisikia kuwa na nguvu kwa kuwa nimeonja asali hii kidogo. Kama tu askari wetu wangeweza kula kidogo kutoka nyara walizoteka kutoka kwa adui zao, wengi zaidi wa Wafilisti wangaliuawa.” Siku ile, Waisraeli waliwapiga Wafilisti, tangu Mikmashi mpaka Aiyaloni. Wakati huu Waisraeli walikuwa wamechoka kwa njaa. Basi walikimbilia nyara walizoteka, wakawachukua wanakondoo, fahali na ndama, wakachinja, wakala nyama na damu. Watu wengine wakamwambia Shauli, “Tazama watu wanatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu kwa kula nyama yenye damu.” Shauli akawaambia watu, “Nyinyi ni wahaini. Vingirisheni jiwe kubwa hapa kwangu.” Akawaambia, “Nendeni mkawaambie watu wote walete ng'ombe na kondoo wao hapa, wawachinje na kuwala hapa. Wasitende dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, kwa kula nyama yenye damu.” Hivyo, usiku ule wote walipeleka ng'ombe wao na kuwachinjia hapo. Basi, Shauli akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu. Hiyo ilikuwa ndiyo madhabahu ya kwanza ambayo Shauli alimjengea Mwenyezi-Mungu. Kisha Shauli akawaambia watu, “Twendeni tukawafuatie Wafilisti usiku, tukawavamie na kupora mali zao mpaka asubuhi; hatutamwacha mtu yeyote hai.” Watu wakamwambia, “Fanya unachoona kuwa chema kwako.” Lakini kuhani akawaambia, “Kwanza tuombe shauri kwa Mwenyezi-Mungu.” Hivyo, Shauli akamwuliza Mungu, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Waisraeli?” Lakini Mungu hakujibu kitu siku hiyo. Shauli akasema, “Njoni hapa enyi viongozi wa watu, tujue ni dhambi gani tumetenda leo. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai na ambaye huiokoa Israeli, hata kama ni mwanangu Yonathani, lazima auawe.” Lakini hakuna mtu aliyesema neno. Hivyo, Shauli akawaambia, “Nyinyi nyote simameni upande ule, halafu mimi na Yonathani mwanangu tutasimama upande huu.” Wao wakajibu, “Fanya chochote unachoona kinafaa.” Shauli akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa Israeli, kwa nini hujanijibu mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu wa Israeli, ikiwa hatia iko kwangu au kwa Yonathani mwanangu, basi, amua kwa jiwe la kauli ya Urimu. Lakini ikiwa hatia hiyo iko kwa watu wako wa Israeli, amua kwa jiwe la kauli ya Thumimu.” Yonathani na Shauli walipatikana kuwa na hatia, lakini watu walionekana hawana hatia. Shauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Yonathani akapatikana kuwa na hatia. Ndipo Shauli akamwambia Yonathani, “Niambie ulilofanya.” Yonathani akajibu, “Nilikula asali kidogo kwa kutumia fimbo yangu. Niko hapa na niko tayari kufa.” Shauli akasema, “Mungu na anitendee mimi vivyo hivyo na hata na wengine. Yonathani ni lazima utauawa.” Lakini watu wakamwambia Shauli, “Mbona Yonathani aliyeiletea Israeli ushindi huu mkubwa, auawe? Jambo hilo liwe mbali. Twaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, hata unywele wa kichwa chake hautaanguka chini. Alichokifanya leo, amekifanya kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu.” Hivyo, watu walimkomboa Yonathani naye hakuuawa. Kisha Shauli aliacha kuwafuatia Wafilisti, nao Wafilisti wakarudi makwao. Baada ya Shauli kuwa mfalme wa Israeli, alipigana na adui zake kila upande: Wamoabu, Waamoni, Waedomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Kila alipopigana vita, alishinda. Alipigana kwa uhodari, akawashinda Waamaleki. Aliwaokoa Waisraeli kutoka kwa watu wote waliowashambulia. Watoto wa kiume wa Shauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-shua. Binti zake walikuwa wawili; mzaliwa wa kwanza aliitwa Merabu na mdogo aliitwa Mikali. Mkewe Shauli aliitwa Ahinoamu binti Ahimaasi. Kamanda wa jeshi la Shauli aliitwa Abneri, mwana wa Neri, mjomba wa Shauli. Baba wa Shauli alikuwa Kishi na baba wa Abneri alikuwa Neri mwana wa Abieli. Kulikuwa na mapigano makali dhidi ya Wafilisti muda wote Shauli alipokuwa mfalme; na kila mara Shauli alipompata mtu mwenye nguvu au shujaa alimchukua ajiunge na jeshi. Samueli alimwambia Shauli, “Mwenyezi-Mungu alinituma kukupaka mafuta uwe mfalme wa watu wake wa Israeli. Sasa sikiliza maneno ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa sababu waliwapiga Waisraeli walipokuwa wanatoka Misri. Sasa, nenda ukawashambulie na kuangamiza vitu vyote walivyo navyo. Usiwaache hai, ila uwaue wote: Wanaume kwa wanawake, watoto wachanga na wanyonyao, ng'ombe, kondoo, ngamia na punda.’” Shauli akaliita jeshi lake, akalikagua huko Telaimu. Kulikuwa na askari wa miguu 200,000 kutoka Israeli na 10,000 kutoka Yuda. Halafu yeye na watu wake wakaenda kwenye mji wa Amaleki, wakawa wakivizia kwenye bonde. Shauli akawaambia Wakeni, “Nendeni! Ondokeni! Tokeni miongoni mwa Waamaleki, la sivyo, nitawaangamiza pamoja nao. Ondokeni kwa sababu nyinyi mliwatendea wema Waisraeli walipotoka Misri.” Basi, Wakeni wakaondoka miongoni mwa Waamaleki. Shauli aliwashinda Waamaleki kuanzia Havila hadi Shuri, mashariki ya Misri. Alimteka mfalme Agagi wa Waamaleki akiwa hai. Akawaua watu kwa makali ya upanga. Lakini Shauli na watu wake hawakumuua Agagi, wala kondoo bora kabisa, ng'ombe wazuri, ndama, wanakondoo na chochote kile kilichokuwa kizuri hawakukiangamiza. Lakini vitu vyote vibaya na visivyo na thamani waliviangamiza. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Ninajuta kwamba nimemfanya Shauli kuwa mfalme. Yeye ameacha kunifuata mimi na hajatimiza amri zangu.” Samueli alikasirika, akamlilia Mwenyezi-Mungu usiku kucha. Samueli alisikia kuwa Shauli alikuwa amekuja huko Karmeli na amesimamisha mnara wa ukumbusho wake, na kwamba amekwenda Gilgali. Hivyo, kesho yake, Samueli aliamka asubuhi na mapema akaenda kukutana na Shauli. Samueli alipomfikia Shauli, Shauli akamwambia Samueli, “Mwenyezi-Mungu na akubariki! Nimetekeleza amri ya Mwenyezi-Mungu.” Samueli akamwambia, “Mbona nasikia mlio wa kondoo na ng'ombe?” Shauli akajibu, “Watu waliwaacha hai kondoo na ng'ombe bora kabisa ili kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, lakini wengine wote tumewaangamiza.” Samueli akamkatiza Shauli, “Nyamaza! Nitakuambia jambo aliloniambia Mwenyezi-Mungu leo usiku.” Shauli akasema, “Niambie.” Samueli akamwambia, “Ingawa unajiona kuwa wewe si maarufu, je, wewe si kiongozi wa makabila ya Israeli? Mwenyezi-Mungu alikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli. Mwenyezi-Mungu alipokutuma alikuambia, ‘Nenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hadi umewaua wote!’ Kwa nini basi, hukuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu? Kwa nini mkakimbilia nyara na hivyo kutenda jambo ovu mbele ya Mwenyezi-Mungu?” Shauli akajibu, “Nimetii sauti ya Mwenyezi-Mungu. Nilikwenda kule alikonituma Mwenyezi-Mungu; nimemleta Agagi mfalme wa Waamaleki, na nimewaangamiza kabisa Waamaleki. Lakini watu walichukua nyara: Kondoo, ng'ombe na vitu vyote bora vilivyotolewa viangamizwe ili kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, huko Gilgali.” Ndipo Samueli akamwambia, “Je, Mwenyezi-Mungu anapendelea zaidi dhabihu za kuteketezwa na matambiko, kuliko kuitii sauti yake? Tazama, kumtii yeye ni bora kuliko matambiko na kumsikiliza kuliko kumtambikia mafuta ya beberu. Uasi ni sawa na dhambi ya kupiga ramli, na kiburi ni sawa na uovu na kuabudu vinyago. Kwa sababu umeikataa amri ya Mwenyezi-Mungu, naye amekukataa kuwa mfalme.” Shauli akamwambia Samueli, “Nimetenda dhambi. Nimeasi amri ya Mwenyezi-Mungu na amri yako, kwa sababu niliwaogopa watu, nikawatii wao. Lakini sasa nakuomba, unisamehe dhambi yangu. Niruhusu nirudi pamoja nawe ili niweze kumwabudu Mwenyezi-Mungu.” Samueli akamjibu: “Kamwe, siwezi kurudi pamoja nawe. Wewe umeikataa amri ya Mwenyezi-Mungu, naye amekukataa kuwa mfalme juu ya Israeli.” Samueli alipogeuka ili aende zake, Shauli akashika pindo la vazi lake, nalo likapasuka. Ndipo Samueli alipomwambia Shauli, “Tangu leo Mwenyezi-Mungu ameurarua ufalme wa Israeli kutoka kwako na atampa mtu mwingine miongoni mwa jirani zako aliye bora kuliko wewe. Na Mungu ambaye ni utukufu wa Israeli hadanganyi, wala habadili wazo lake. Yeye si binadamu hata abadili mawazo.” Shauli akajibu, “Nimefanya dhambi. Hata hivyo, unistahi sasa mbele ya wazee wa watu wangu na Waisraeli. Niruhusu nirudi pamoja nawe ili nikamwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.” Basi, Samueli akarudi pamoja naye mpaka Gilgali na Shauli akamwabudu Mwenyezi-Mungu. Kisha Samueli akasema, “Nileteeni hapa Agagi mfalme wa Waamaleki.” Agagi akamwendea Samueli akiwa mwenye furaha kwani alifikiri, “Uchungu wa kifo umepita.” Samueli akasema, “Kwa kuwa upanga wako umewafanya akina mama wengi wasiwe na watoto, ndivyo na mama yako atakavyokuwa bila mtoto miongoni mwa akina mama.” Akamkatakata Agagi vipandevipande mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Gilgali. Kisha, Samueli akaenda Rama; na mfalme Shauli akarudi nyumbani kwake huko Gibea. Tangu siku hiyo, Samueli hakumwona tena Shauli, mpaka siku alipofariki. Hata hivyo Samueli alimlilia Shauli. Naye Mwenyezi-Mungu alisikitika kwamba alikuwa amemtawaza Shauli mfalme juu ya Israeli. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Utamlilia Shauli mpaka lini? Wewe unajua kuwa mimi nimemkataa kuwa mfalme juu ya Israeli. Sasa, jaza upembe wako mafuta, uondoke. Nitakutuma kwa Yese wa mji wa Bethlehemu. Maana nimejipatia mfalme miongoni mwa wanawe.” Samueli akasema, “Nitawezaje kwenda? Kama Shauli akisikia habari hizo, ataniua!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Chukua ndama pamoja nawe, na ukifika huko useme, ‘Nimekuja kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko’. Mwalike Yese kwenye tambiko hiyo nami nitakuonesha la kufanya. Utampaka mafuta kwa ajili yangu mtu yule nitakayekutajia.” Samueli akafanya kama alivyoambiwa na Mwenyezi-Mungu, akaenda Bethlehemu. Wazee wa mji wakatoka kumlaki wakiwa wanatetemeka, wakamwuliza, “Je, umekuja kwa amani?” Samueli akawaambia, “Nimekuja kwa amani. Nimekuja kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Jitakaseni wenyewe halafu twendeni kutoa tambiko.” Samueli akamtakasa Yese pamoja na wanawe, akawakaribisha kwenye tambiko. Walipofika, na Samueli alipomwona Eliabu, alijisemea moyoni mwake, “Hakika, mpakwa mafuta wa Mwenyezi-Mungu ndiye huyu aliye mbele ya Mwenyezi-Mungu!” Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiangalie sura yake na urefu wa kimo chake. Mimi nimemkataa kwani siangalii mambo kama wanavyoyaangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni.” Kisha, Yese akamwita Abinadabu na kumleta mbele ya Samueli. Lakini Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.” Yese akamleta Shama. Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.” Yese aliwapitisha wanawe wote saba mbele ya Samueli lakini Samueli akamwambia, “Mwenyezi-Mungu hajamchagua yeyote kati ya hawa.” Halafu akamwambia, “Je, wanao wote wako hapa?” Yese akajibu, “Bado yuko mdogo, lakini amekwenda kuchunga kondoo.” Samueli akamwambia, “Mtume mtu amlete; sisi hatutaketi chini, mpaka atakapokuja hapa.” Hivyo, Yese alituma mtu, naye akaletwa. Yule kijana alikuwa mwenye afya, mwenye macho maangavu na wa kupendeza. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Sasa, huyu ndiye; inuka umpake mafuta.” Samueli akachukua upembe wake wenye mafuta akammiminia Daudi mafuta mbele ya kaka zake. Mara roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Daudi kwa nguvu, ikakaa tangu siku hiyo na kuendelea. Kisha Samueli akarudi mjini Rama. Baadaye roho ya Mwenyezi-Mungu ilimwacha Shauli, na roho mwovu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ikamsumbua. Ndipo watumishi wake Shauli wakamwambia, “Tunajua kwamba roho mwovu kutoka kwa Mungu anakusumbua. Sasa, ee bwana wetu, amuru watumishi wako wanaokutumikia wamtafute mtu mwenye ufundi wa kupiga kinubi, na huyo roho mwovu kutoka kwa Mungu atakapokujia, mtu huyo atapiga kinubi, nawe utapata nafuu.” Shauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mtu huyo anayeweza kupiga kinubi vizuri, mniletee.” Kijana mmoja miongoni mwa watumishi akasema, “Nimemwona kijana mmoja wa Yese, wa mji wa Bethlehemu. Kijana huyo ana ujuzi wa kupiga kinubi. Huyo kijana ni shujaa, hodari wa kupigana vitani, ana busara katika kusema na mwenye umbo zuri; Mwenyezi-Mungu yuko pamoja naye.” Hivyo, Shauli alituma ujumbe kwa Yese, na kusema, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.” Yese alimtuma Daudi kwa Shauli pamoja na punda aliyebeba mikate, kiriba cha divai na mwanambuzi. Daudi alipofika akaingia kumtumikia Shauli. Shauli alimpenda sana, hata akamfanya awe mwenye kumbebea silaha zake. Halafu Shauli alituma ujumbe kwa Yese na kusema, “Nampenda Daudi; mwache akae hapa anitumikie.” Kila mara, yule roho mwovu kutoka kwa Mungu alipomjia Shauli, Daudi alichukua kinubi chake na kuanza kukipiga, na roho huyo alimwacha Shauli, naye akaburudika na kupata nafuu. Sasa, Wafilisti walikusanya majeshi yao huko Soko, mji ulioko katika Yuda, tayari kwa vita. Walipiga kambi katika sehemu moja iitwayo Efes-damimu kati ya Soko na Azeka. Shauli pamoja na Waisraeli walikusanyika, na kupiga kambi katika bonde la Ela. Wakajipanga tayari kupigana na Wafilisti. Wafilisti walisimama mlimani upande mmoja na Waisraeli walisimama mlimani upande mwingine, katikati yao kulikuwa na bonde. Kutoka kwenye kambi ya Wafilisti, alijitokeza shujaa mmoja aitwaye Goliathi, mwenyeji wa mji wa Gathi. Urefu wake ulikaribia mita tatu. Kichwani alivaa kofia ya shaba, na deraya ya shaba kifuani yenye uzito wa kilo 57. Miguu yake pia ilikuwa na kinga ya shaba na mabegani pake alibeba mkuki wa shaba. Mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumanguo, na chembe cha mkuki huo, kilikuwa na uzito wa kilo saba. Ngao yake ilibebwa na mtu mwingine aliyemtangulia. Goliathi alisimama na kuwapigia kelele wanajeshi wa Israeli, akisema, “Mnafanya nini hapo? Je, mmekuja kupigana vita? Mimi ni Mfilisti, nyinyi ni watumwa wa Shauli. Chagueni mtu mmoja wenu aje kupigana nami. Akinishinda na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu. Lakini nikimshinda na kumuua basi, nyinyi mtakuwa watumwa wetu na kututumikia.” Kisha Mfilisti huyo aliendelea kusema kwa majivuno, “Nawataka wanajeshi wa Israeli siku hii kumtoa mtu mmoja aje kupigana nami.” Shauli pamoja na wanajeshi wote wa Israeli walipoyasikia maneno hayo ya Mfilisti huyo, walifadhaika na kuogopa sana. Daudi alikuwa mtoto wa Yese, Mwefrathi kutoka Bethlehemu katika Yuda. Yese alikuwa na watoto wanane wa kiume. Wakati Shauli alipokuwa mfalme, yeye alikuwa tayari mzee, mtu mwenye umri mkubwa. Wana wakubwa watatu wa Yese, Eliabu mzaliwa wa kwanza, Abinadabu aliyefuata na Shama wa tatu, walikuwa wamekwenda pamoja na Shauli vitani. Daudi alikuwa ndiye mdogo wa wote. Wale watoto watatu wakubwa walikuwa wamekwenda na Shauli. Ingawa Daudi mara kwa mara alikwenda kwa Shauli, alirudi nyumbani Bethlehemu kuchunga kondoo wa baba yake. Kwa muda wa siku arubaini, asubuhi na jioni, yule Mfilisti Goliathi alijitokeza hadharani, akasimama na kuwakejeli wanajeshi wa Israeli. Siku moja, Yese alimwambia mwanawe Daudi, “Wapelekee kaka zako bisi kilo kumi na mikate kumi. Wapelekee haraka huko kambini. Na yule kamanda wao wa kikosi cha wanajeshi elfu mpelekee jibini hizi kumi. Kawaangalie kaka zako kama wanaendelea vizuri na kisha uniletee habari zao.” Wakati huo mfalme Shauli, kaka zake Daudi na wanajeshi wote wa Israeli walikuwa kwenye bonde la Ela, wanapigana na Wafilisti. Kesho yake, Daudi aliamka asubuhi na mapema, na kondoo akamwachia mchungaji. Alichukua chakula na kwenda kama alivyoagizwa na baba yake Yese. Alipofika kwenye kambi ya Waisraeli, aliwakuta wanajipanga kwenye sehemu yao ya vita na wanapiga kelele za vita. Majeshi ya Waisraeli na ya Wafilisti walijipanga tayari kupigana vita, majeshi yakiwa yanakabiliana ana kwa ana. Daudi alimkabidhi chakula mtu aliyetunza mizigo, akawakimbilia wanajeshi, akaenda kwa kaka zake na kuwasalimia. Alipokuwa anaongea nao, Goliathi yule shujaa wa Wafilisti kutoka Gathi alijitokeza mbele ya wanajeshi wa Israeli kama alivyozoea. Naye Daudi alimsikiliza vizuri sana. Waisraeli walipomwona Goliathi, walimkimbia, na kumwogopa sana. Waliambiana, “Je, mmemwona yule mtu aliyejitokeza? Ama kweli, amejitokeza kuwakejeli Waisraeli. Mfalme Shauli atampa mtu yeyote atakayemuua mtu huyo utajiri mwingi. Zaidi ya yote, atamwoza binti yake. Tena, watu wa jamaa ya baba yake watakuwa huru, hawatalipa kodi.” Daudi akawauliza wale waliokuwa karibu naye, “Je, mtu atakayemuua Mfilisti huyu na kuikomboa Israeli kutokana na aibu hii atafanyiwa nini? Ni nani huyu Mfilisti, mtu asiyetahiriwa, anayethubutu kuyatukana majeshi ya Mungu aliye hai?” Watu wakamwambia kama walivyokuwa wamesema hapo awali juu ya mtu atakayemuua Goliathi. Lakini Eliabu, kaka mkubwa wa Daudi alipomsikia Daudi akiongea na watu, alimkasirikia Daudi, akasema, “Kwa nini umekuja? Je, wale kondoo wachache umemwachia nani kule nyikani? Najua ujeuri wako na uovu wako. Umekuja tu kutazama vita.” Daudi akamjibu, “Sasa nimefanya nini? Je, siwezi kuuliza swali tu?” Daudi akamgeukia mtu mwingine akamwuliza swali hilohilo; na kila alipouliza, alipata jibu lilelile. Watu fulani ambao walimsikia Daudi alivyosema, walikwenda kumwambia Shauli. Naye Shauli akaagiza aitwe. Daudi akamwambia Shauli, “Mtu yeyote asitishike moyoni mwake kutokana na Mfilisti huyu. Mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana naye.” Shauli akamwambia Daudi, “Wewe huwezi kwenda kupigana na Mfilisti yule. Wewe ni kijana tu, lakini mtu huyo amekuwa vitani tangu ujana wake.” Daudi akasema, “Mimi mtumishi wako nimezoea kuchunga kondoo wa baba yangu. Kila wakati simba au dubu akija na kukamata mwanakondoo mimi humfuata na kumshambulia, nikamwokoa mwanakondoo kinywani mwake. Kama simba au dubu akinishambulia, mimi humshika ndevu zake, nikamwangusha na kumuua. Mimi mtumishi wako nimekwisha ua simba wengi na dubu wengi. Sasa, hata yule Mfilisti asiyetahiriwa, ambaye ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai, atakuwa kama hao. Mwenyezi-Mungu ambaye ameniokoa makuchani mwa simba na dubu, ataniokoa kutoka kwa Mfilisti huyu.” Shauli akamwambia, “Nenda; naye Mwenyezi-Mungu awe pamoja nawe.” Shauli akamvisha Daudi mavazi yake ya kivita, akamvika kofia yake ya shaba kichwani na koti lake la kujikinga kifua. Daudi akajifunga upanga wa Shauli, akajaribu kutembea; lakini akashindwa kwa kuwa hakuyazoea mavazi kama hayo. Akamwambia Shauli, “Siwezi kwenda vitani nikiwa nimevaa mavazi haya, kwani mimi sijayazoea.” Kwa hiyo, akayavua. Daudi akachukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe matano mazuri kutoka kwenye kijito, akayatia katika mfuko wake wa mchungaji. Kombeo lake likiwa tayari mkononi mwake, akaanza kumwendea Goliathi Mfilisti. Yule Mfilisti, naye akaanza kumwendea Daudi, na yule aliyemchukulia ngao yake akiwa mbele yake. Yule Mfilisti alipoangalia na kumwona vizuri Daudi, alimdharau, kwani Daudi alikuwa kijana tu, mwenye afya na wa kupendeza. Goliathi akamwuliza Daudi, “Sasa, hiyo fimbo ni ya nini? Unadhani mimi ni mbwa hata unijie kwa fimbo?” Mfilisti huyo akamlaani Daudi kwa miungu yake. Mfilisti akamwambia Daudi, “Njoo kwangu! Mwili wako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini!” Lakini Daudi akamwambia Goliathi, “Wewe unanijia kwa upanga, mkuki na sime. Lakini mimi ninakujia kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa askari wa Israeli, ambaye wewe umemtukana. Siku ya leo, Mwenyezi-Mungu atakutia mikononi mwangu. Nitakubwaga chini, nitakukata kichwa chako; na miili ya wanajeshi wa Wafilisti nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini. Ndipo dunia nzima itakapojua kuwa Mungu yuko katika Israeli. Watu wote waliokusanyika hapa leo, watajua kuwa Mwenyezi-Mungu hahitaji mikuki wala sime kuwaokoa watu. Hii ni vita ya Mwenyezi-Mungu, naye atawatia nyinyi nyote mikononi mwetu.” Goliathi akaanza tena kumwendea Daudi. Daudi akakimbia mbio kwenda kwenye mstari wa mapambano. Akatia mkono wake mfukoni mwake, akatoa jiwe moja, akalirusha kwa kombeo lake, akampiga nalo Goliathi kwenye paji la uso wake, jiwe likalipasua paji la Goliathi na kupenya ndani. Goliathi akaanguka chini kifudifudi. Ndivyo Daudi alivyomshinda Goliathi kwa kombeo lake na jiwe. Alimpiga yule Mfilisti na kumuua. Daudi hakuwa na upanga wowote mkononi mwake. Basi, akaenda mbio, akasimama juu ya Goliathi, akaufuta upanga wa Goliathi alani mwake, akamuua Goliathi kwa kumkata kichwa chake. Wafilisti walipoona kuwa shujaa wao ameuawa, wakatimua mbio. Ndipo watu wa Israeli na watu wa Yuda, walipoanza kupiga kelele za ushindi, wakawafuatilia Wafilisti hadi Gathi, kwenye malango ya Ekroni, hata Wafilisti waliojeruhiwa vitani walienea njiani tangu Shaarimu hadi Gathi na Ekroni. Waisraeli walipotoka kuwafuatilia Wafilisti, waliteka nyara kambi yao. Daudi alikichukua kichwa cha yule Goliathi, Mfilisti, akakipeleka mjini Yerusalemu. Lakini silaha za Goliathi akaziweka katika hema lake. Shauli alipomwona Daudi akienda kumkabili yule Mfilisti Goliathi, alimwuliza Abneri, kamanda wa jeshi lake, “Abneri, huyu ni kijana wa nani?” Abneri alijibu, “Mfalme, kama uishivyo, mimi sijui.” Mfalme Shauli akamwambia, “Basi, uliza yeye ni kijana wa nani.” Mara tu Daudi aliporudi kambini baada ya kumuua Goliathi, Abneri alimchukua na kumpeleka kwa Shauli. Wakati huo Daudi alikuwa bado amechukua kichwa cha Goliathi mikononi mwake. Shauli akamwuliza Daudi, “Kijana, wewe ni mwana wa nani?” Daudi akajibu, “Mimi ni mwana wa mtumishi wako Yese, kutoka mji wa Bethlehemu.” Shauli alipomaliza kuzungumza na Daudi, Yonathani mwana wa Shauli, alivutiwa sana na Daudi, akampenda kwa moyo wake wote kama alivyojipenda yeye mwenyewe. Tangu siku hiyo, Shauli akamchukua Daudi nyumbani kwake, asimruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake. Kwa kuwa Yonathani alimpenda Daudi kama roho yake, alifanya agano naye. Alivua vazi alilovaa na kumpa Daudi pamoja na silaha zake, hata upanga, upinde na mkanda wake. Kokote Daudi alikotumwa na Shauli, Daudi alifanikiwa. Hivyo, Shauli akamfanya kuwa mkuu wa jeshi lake. Jambo hilo liliwafurahisha watu wote hata watumishi wa Shauli. Askari walipokuwa wanarudi nyumbani, pamoja na Daudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake kutoka kila mji katika Israeli walitoka kwenda kumlaki mfalme Shauli. Wanawake nao walikuwa wanaimba nyimbo za furaha, wakipiga matari na vinubi. Pia walikuwa wanacheza na kuimba nyimbo za kuitikiana hivi: “Shauli ameua maelfu yake, na Daudi ameua makumi elfu yake.” Shauli hakupendezwa na maneno ya wimbo huo, hivyo akakasirika sana. Akasema, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa maelfu tu. Lililobakia ni kumpa Daudi ufalme.” Tangu siku hiyo, Shauli akawa anamwonea kijicho Daudi. Kesho yake, roho mwovu kutoka kwa Mungu, alimvamia Shauli kwa ghafla, akawa anapayukapayuka kama mwendawazimu nyumbani kwake. Daudi alikuwa anapiga kinubi kama alivyofanya siku zote. Shauli alikuwa na mkuki mkononi mwake; basi, alimtupia Daudi mkuki mara mbili kwani alifikiri, “Nitambana Daudi ukutani.” Lakini Daudi alikwepa mara zote mbili. Shauli alikuwa anamwogopa Daudi kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye, lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwacha Shauli. Hivyo, Shauli akamwondoa na kumfanya kiongozi wa wanajeshi 1,000. Naye Daudi akawaongoza vyema vitani. Daudi alifanikiwa katika kila kitu alichofanya, kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye. Shauli alipoona kufanikiwa kwa Daudi, akawa anamwogopa. Lakini watu wote wa Israeli na Yuda walimpenda Daudi, kwani aliwaongoza vizuri vitani na kuwarudisha kwa mafanikio. Shauli akamwambia Daudi, “Huyu ni Merabu, binti yangu mkubwa, nitakuoza awe mke wako kwa masharti mawili: Uwe askari wangu shupavu na mtiifu, upigane vita vya Mwenyezi-Mungu.” [Shauli alidhani kwa njia hiyo Wafilisti watamuua Daudi, ili kitendo hicho asikifanye yeye mwenyewe.] Daudi akamwambia Shauli, “Mimi ni nani hata mfalme awe baba mkwe wangu? Ukoo wangu wenyewe na hata jamaa ya baba yangu si maarufu katika Israeli.” Lakini, wakati ule ambapo Merabu binti yake Shauli angeozwa kwa Daudi, aliozwa kwa Adrieli kutoka mji wa Mehola. Hata hivyo, Mikali binti mwingine wa Shauli alimpenda Daudi. Shauli alipoambiwa alifurahi sana. Shauli alifikiri, “Ngoja nimwoze huyu ili awe mtego kwake. Na bila shaka Wafilisti watamuua.” Hivyo Shauli akamwambia Daudi mara ya pili, “Sasa nitakuwa baba mkwe wako.” Halafu Shauli aliwaamuru watumishi wake akisema “Ongea faraghani na Daudi na kumwambia, ‘Mfalme anapendezwa sana nawe, hata watumishi wake pia wote wanakupenda’. Hivyo, sasa kubali kuwa mkwewe mfalme.” Basi, watumishi hao wa Shauli walimwambia Daudi maneno hayo faraghani, naye akawaambia, “Mimi ni mtu maskini na duni. Je mnadhani mfalme kuwa baba mkwe wangu ni jambo rahisi?” Wale watumishi walimweleza Shauli kama Daudi alivyosema. Shauli akawaambia, “Mwambieni Daudi hivi: ‘Kile ambacho mfalme anataka kama mahari ya binti yake ni magovi 100 ya Wafilisti, ili ajilipize kisasi cha adui zake.’” [Hivi ndivyo Shauli alivyopanga Daudi auawe na Wafilisti.] Wale watumishi walipomweleza Daudi yale matakwa ya Shauli, Daudi alifurahi kuwa mfalme atakuwa baba mkwe wake. Kabla ya siku ya harusi, Daudi na watu wake walikwenda, wakawaua Wafilisti 200 na kuyachukua magovi yao mpaka kwa mfalme Shauli. Hapo akamhesabia idadi kamili ili mfalme awe baba mkwe wake Daudi. Hivyo, Shauli akamwoza Daudi binti yake Mikali awe mke wake. Lakini Shauli alipoona wazi kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Daudi, na kuwa Mikali binti yake alimpenda mno Daudi, alizidi kumwogopa Daudi. Shauli akawa adui wa Daudi daima. Jeshi la Wafilisti lilikwenda kupigana na Waisraeli, lakini kila mara walipopigana vita, Daudi alipata ushindi kuliko watumishi wa Shauli; hivyo jina lake Daudi likazidi kusifiwa sana. Shauli alimweleza mwanawe Yonathani na maofisa wake juu ya mpango wake wa kumwua Daudi. Lakini Yonathani, mwanawe Shauli, alimpenda sana Daudi. Kwa hiyo, akamwambia, “Baba yangu anakusudia kukuua. Hivyo, jihadhari. Kesho asubuhi, jifiche mahali pa siri, ukae hapo. Mimi nitakuja na kusimama karibu na baba yangu huko shambani mahali utakapokuwa. Hapo nitaongea naye juu yako, na kitu chochote nitakachogundua kutoka kwake, nitakueleza.” Yonathani alimsifu Daudi mbele ya baba yake, akamwambia, “Usitende dhambi dhidi ya mtumishi wako Daudi kwani yeye hajatenda dhambi yoyote dhidi yako; matendo yake yote anapokutumikia daima yamekuwa mema kwako. Alipomuua yule Mfilisti Goliathi, alihatarisha maisha yake, naye Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli ushindi mkubwa. Wewe ulipoona jambo lile ulifurahi. Kwa nini unataka kutenda dhambi kwa kumwaga damu isiyo na hatia kwa kumwua Daudi bila sababu?” Shauli alimsikiliza Yonathani, kisha akaapa, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, sitamuua Daudi.” Hivyo, Yonathani akamwita Daudi na kumweleza mambo hayo yote. Yonathani akampeleka Daudi kwa Shauli, na Daudi akamtumikia Shauli kama hapo awali. Baadaye kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Waisraeli. Daudi alitoka akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na waliosalia wakamkimbia. Kisha, roho mbaya kutoka kwa Mwenyezi-Mungu alimjia Shauli alipokuwa amekaa nyumbani kwake akiwa ameshika mkuki mkononi, wakati ambapo Daudi alikuwa akipiga kinubi. Shauli alijaribu kumchoma Daudi kwa mkuki huo, Lakini Daudi alikwepa mkuki wa Shauli na mkuki ukapiga ukuta. Daudi akakimbia na kutoroka. Usiku huo, Shauli alituma watu nyumbani kwa Daudi wamwangalie kama yuko ili apate kumwua asubuhi. Lakini Mikali, mke wa Daudi akamwambia Daudi, “Kama huyasalimishi maisha yako usiku huu kesho utauawa.” Hivyo Mikali akamteremsha Daudi kupitia dirishani, naye akatoka na kutoroka. Mikali akachukua kinyago, akakilaza kitandani na kichwani pake akaweka mto wa manyoya ya mbuzi. Kisha akakifunika kwa nguo. Shauli alipotuma watu kumshika Daudi, Mikali akawaambia kuwa Daudi ni mgonjwa. Kisha Shauli aliwatuma warudi huko tena, akawaagiza akisema, “Mlete kwangu Daudi hata akiwa kitandani ili auawe.” Wale watu walipoingia nyumbani kwa Daudi na kukiangalia kitanda waliona kuna kinyago na mto wa manyoya ya mbuzi kichwani. Halafu Shauli akamwuliza Mikali, “Kwa nini umenidanganya? Umemwacha adui yangu atoroke?” Naye Mikali akamjibu Shauli, “Aliniambia, ‘Niache niende nisije nikakuua.’” Daudi alipotoroka, alikwenda Rama kwa Samueli. Alimweleza Samueli mambo yote aliyomfanyia Shauli. Basi, Daudi na Samueli walikwenda na kukaa huko Nayothi. Baadaye Shauli aliambiwa kuwa Daudi alikuwa huko Nayothi katika Rama. Ndipo Shauli alipopeleka watu wakamkamate. Lakini walipolikuta kundi la manabii likitabiri na Samueli akiliongoza, roho ya Mungu iliwajia wale watumishi wa Shauli, nao pia wakaanza kutabiri. Shauli alipoambiwa habari hizo, alituma watumishi wengine, nao pia wakaanza kutabiri. Shauli alipotuma watumishi wengine kwa mara ya tatu, nao pia wakaanza kutabiri. Ndipo yeye mwenyewe akaenda Rama. Alipofika kwenye kisima kikubwa kilichoko huko Seku, alimkuta mtu fulani ambaye alimwuliza, “Samueli na Daudi wako wapi?” Huyo mtu alimjibu, “Wako Nayothi, katika Rama.” Naye Shauli akaenda huko Nayothi katika Rama. Alipofika huko, roho ya Mungu ilimjia, naye alianza kutabiri akiwa njiani mpaka alipofika Nayothi katika Rama. Alivua mavazi yake akawa anatabiri mbele ya Samueli. Alibaki uchi kwa siku moja, mchana na usiku. Kwa hiyo watu walianza kujiuliza, “Je, Shauli naye pia amekuwa mmoja wa manabii?” Daudi alikimbia kutoka Nayothi katika Rama, akaenda mpaka kwa Yonathani, akamwambia, “Nimefanya nini? Kosa langu ni nini? Nimemtendea baba yako dhambi gani hata ajaribu kuyaangamiza maisha yangu?” Yonathani akamjibu, “Hilo na liwe mbali nawe. Hutakufa. Baba yangu hafanyi jambo lolote, liwe kubwa au dogo, bila ya kunieleza. Hata jambo hili hawezi kunificha. Sivyo ilivyo hata kidogo.” Daudi akaapa pia, “Hakika baba yako anajua vizuri unavyonipenda; na anafikiri kukuficha juu ya jambo hili ili usihuzunike atakapolitenda. Lakini, kwa vyovyote vile, naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, nawe ulivyo hai, kwamba kati yangu na mauti ipo hatua moja tu!” Yonathani akamwambia, “Lolote utakalosema nitakutendea.” Daudi akamwambia, “Kesho ni sherehe za mwezi mwandamo, nami natazamiwa kuwapo mezani kula pamoja na mfalme. Lakini niache, nikajifiche huko shambani hadi siku ya tatu jioni. Baba yako akinikosa mezani kwa chakula, akauliza habari zangu, basi mwambie, ‘Daudi amenisihi nimpe ruhusa ili aende mjini kwake Bethlehemu, kuhudhuria tambiko ya kila mwaka pamoja na jamaa yake’. Ikiwa ataona hilo ni sawa, basi, ujue kuwa mambo yangu, mimi mtumishi wako, yako sawa. La sivyo, kusudi lake juu yangu ni baya. Hivyo nifanyie kwa hisani yako kwani umefanya agano takatifu nami, mimi mtumishi wako, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Lakini, kama nimefanya kosa basi, na uniue wewe mwenyewe; kwa nini unipeleke kwa baba yako ili aniue?” Yonathani akamjibu, “Wazo hilo na liwe mbali nawe. Hakika, kama ningejua kuwa baba yangu amekusudia mabaya juu yako nisingekuficha.” Daudi akauliza, “Nitajuaje ikiwa baba yako atakujibu kwa ukali?” Yonathani akamjibu, “Njoo twende shambani!” Basi, wakaenda. Yonathani akamwambia Daudi, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, na awe shahidi yetu. Kesho au kesho kutwa, wakati kama huu nitamwuliza baba yangu. Ikiwa msimamo wake juu yako ni mzuri nitakueleza. Mwenyezi-Mungu na aniue ikiwa Shauli anakusudia kukudhuru, nami nisikutahadharishe ili uende mahali mbali ambapo utakuwa salama. Mwenyezi-Mungu na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu. Ikiwa nitaendelea kuwa hai basi, nioneshe ule upendo thabiti wa Mwenyezi-Mungu, ili nisife, tena usiache kuitendea jamaa yangu kwa uaminifu milele. Na Mwenyezi-Mungu atakapowakatilia mbali adui zako kutoka duniani, naomba na jina langu lisikatiliwe mbali kutoka jamaa yako. Mwenyezi-Mungu awalipize kisasi adui zako.” Kwa mara nyingine tena, Yonathani alimwambia Daudi aape kulingana na upendo wake kwake yeye Yonathani, kwani alimpenda Daudi kama alivyoipenda roho yake. Kisha akamwambia Daudi, “Kwa kuwa kesho ni sherehe za mwezi mwandamo, watu wataona wazi kwamba hupo, kwani kiti chako kitakuwa wazi. Tena, kesho kutwa, watu watakukosa kabisa. Siku hiyo nenda mahali ambapo ulijificha wakati jambo hili lilipokuwa bado motomoto, ukajifiche nyuma ya rundo la mawe. Mimi nitapiga mishale mitatu kandokando kana kwamba ninalenga shabaha fulani. Nitamtuma mtumishi wangu aende kuitafuta mishale hiyo. Kama nikimwambia, ‘Tazama, mishale hiyo iko upande huo wako, ichukue,’ hiyo itakuwa na maana kwamba uko salama, nawe utajitokeza kutoka mahali ulipojificha, maana naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba utakuwa salama bila hatari yoyote. Lakini nikimwambia, ‘Tazama, mishale iko mbele yako,’ hapo, ondoka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu atakuwa anataka uende mbali. Kulingana na ahadi tulizowekeana, Mwenyezi-Mungu atakuwa shahidi kati yetu milele.” Basi, Daudi akajificha shambani. Wakati wa sherehe za mwezi mwandamo, mfalme Shauli akaketi mezani kula. Kama ilivyokuwa kawaida yake, mfalme aliketi kwenye kiti chake kilichokuwa karibu ukutani. Yonathani akaketi mkabala na mfalme na Abneri akaketi karibu na mfalme. Lakini mahali pa Daudi pakawa wazi. Siku hiyo, Shauli hakusema lolote, kwani alifikiri kuwa labda Daudi amepatwa na tatizo au yeye si safi kuhudhuria sherehe hiyo. Siku ya pili, baada ya sherehe za mwezi mwandamo, bado mahali pa Daudi palikuwa wazi. Shauli akamwuliza mwanawe Yonathani, “Kwa nini Daudi mwana wa Yese, hakuja kwenye chakula, jana na leo?” Yonathani akamjibu, “Alinisihi sana nimruhusu aende Bethlehemu. Aliniambia, ‘Niruhusu niende kwa jamaa yangu, kwa kuwa wanafanya karamu ya tambiko huko mjini, na ndugu yangu amenitaka niwepo. Hivyo kama ni sawa kwako niruhusu niende kwa ndugu zangu’. Ndio maana hayuko hapa kushiriki chakula cha mfalme.” Hapo Shauli akawaka hasira dhidi ya Yonathani, akamwambia, “Mwana wa mwanamke mpotovu na mwasi wewe! Ninajua kuwa umejichagulia mwana wa Yese kwa aibu yako mwenyewe, na kumwaibisha mama yako! Je, hujui kwamba Daudi awapo hai, wewe hutaweza kupata fursa ya kuwa mfalme wa nchi hii? Sasa nenda ukamlete hapa kwangu, kwa kuwa lazima auawe.” Yonathani akamjibu, “Kwa nini auawe? Amefanya nini?” Lakini Shauli mara akamtupia Yonathani mkuki ili amuue. Naye Yonathani akatambua kuwa baba yake alikuwa amepania kumwua Daudi. Hapo Yonathani, huku akiwa amekasirika sana, aliondoka mezani kwa haraka, wala hakula chakula chochote siku hiyo ya pili ya sherehe za mwezi mwandamo. Yonathani alihuzunika sana juu ya Daudi kwa sababu baba yake alikuwa amemwaibisha. Kesho yake asubuhi, Yonathani alikwenda kule shambani, kukutana na Daudi kama walivyoagana. Alikwenda huko na kijana mmoja wa kiume. Alipofika huko alimwambia yule kijana wake, “Kimbia ukaitafute mishale ambayo nitapiga.” Yule kijana alipokuwa anakimbia, Yonathani akapiga mshale mbele yake. Yule kijana alipofika mahali ambapo mshale uliangukia, Yonathani akamwita, “Mshale uko mbele yako. Fanya haraka na usisimame tu mahali hapo.” Yule kijana alikusanya mishale na kumwendea bwana wake. Lakini yule kijana hakujua chochote juu ya maana ya kitendo hicho. Waliojua ni Yonathani na Daudi tu. Yonathani akamkabidhi yule kijana silaha zake na kumwambia “Nenda urudi mjini.” Mara yule kijana alipokwisha ondoka, Daudi akainuka na kutoka mahali alipojificha karibu na rundo la mawe. Aliinama chini kwa heshima mara tatu mbele ya Yonathani. Wote wawili, Daudi na Yonathani, wakakumbatiana na kulia. Daudi alikuwa na uchungu zaidi kuliko Yonathani. Halafu Yonathani akamwambia Daudi, “Nenda kwa amani. Tumekwisha apa wote kwa jina la Mwenyezi-Mungu, kuwa Mwenyezi-Mungu awe shahidi kati yetu milele, na kati ya wazawa wangu na wazawa wako milele.” Daudi akainuka na kwenda zake, naye Yonathani akarudi mjini. Daudi alikwenda kwa kuhani Ahimeleki huko Nobu. Ahimeleki akatoka kumlaki huku akiwa anatetemeka, akamwuliza, “Kwa nini umekuja hapa peke yako?” Daudi akamjibu, “Niko hapa kutokana na amri ya mfalme. Aliniambia nisimweleze mtu yeyote juu ya kile ambacho amenituma. Nimeagana na watu wangu kwamba tukutane mahali fulani. Je, una kitu chochote? Nakuomba mikate mitano au chochote kilichoko.” Kuhani Ahimeleki akamwambia, “Hapa sina mkate wa kawaida. Ninayo tu ile mikate mitakatifu. Mnaweza kupewa mikate hiyo ikiwa watu wako hawajalala na wanawake hivi karibuni.” Daudi akamwambia, “Kwa hakika, daima ninapokwenda kwa ajili ya shughuli maalumu, wanawake wamekuwa mbali nasi! Ikiwa miili ya vijana wangu ni mitakatifu tuwapo kwenye shughuli za kawaida, je, si zaidi katika shughuli hii maalumu?” Hivyo kuhani Ahimeleki akampa mikate mitakatifu, kwani hapakuwa na mikate mingine isipokuwa hiyo ya kuwekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu, ikabadilishwa na mikate mipya kutoka mekoni. Basi kulikuwa hapo siku hiyo mtumishi mmoja wa Shauli ambaye alikuwa amezuiliwa mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mtumishi huyo aliitwa Doegi, Mwedomu, msimamizi wa wachungaji wa Shauli. Basi, Daudi akamwambia Ahimeleki, “Je, una upanga au mkuki ambao unaweza kunipatia? Kwa kuwa shughuli za mfalme zilinilazimu niondoke haraka, nami niliondoka bila upanga wangu wala silaha nyingine yoyote.” Ahimeleki akamjibu, “Ninao ule upanga wa Mfilisti Goliathi uliyemuua kwenye bonde la Ela; uko nyuma ya kizibao cha kuhani umefungwa katika kitambaa. Ikiwa unataka kuuchukua huo basi, uchukue kwani hakuna upanga mwingine hapa.” Daudi akamwambia, “Hakuna upanga mwingine kama huo; nakuomba unipe.” Siku hiyo, Daudi alimkimbia Shauli, akaenda kwa mfalme Akishi wa Gathi. Watumishi wa mfalme wakamwambia Akishi, “Huyu si Daudi, mfalme wa nchi ya Israeli? Je, si huyu ambaye walikuwa wakiimbiana juu yake katika ngoma, wakisema, ‘Shauli ameua maelfu yake na Daudi ameua makumi elfu yake?’” Maneno hayo Daudi hakuweza kuyasahau, akaanza kumwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi. Hivyo, akabadilisha tabia yake, akijifanya mwendawazimu, akawa anakwaruzakwaruza kwenye malango ya mji, na mate yake akayaacha yatiririke kwenye ndevu zake. Akishi akawaambia watumishi wake, “Mnajua kuwa mtu huyu ni mwendawazimu; kwa nini mmemleta kwangu? Je, nawahitaji wendawazimu zaidi? Kwa nini mnaniletea mwendawazimu aje kunisumbua na vitendo vya wendawazimu? Je, mtu huyu ataingia nyumbani kwangu?” Daudi aliondoka huko akakimbilia kwenye pango karibu na mji wa Adulamu. Kaka zake na ndugu zake wengine waliposikia kwamba alikuwa hapo, wote walikwenda kuungana naye. Watu wote waliokandamizwa au waliokuwa na madeni, au wale ambao hawakuridhika walijumuika na Daudi. Jumla yao ilikuwa watu kama 400, naye akawa kiongozi wao. Kutoka huko, Daudi alikwenda mpaka huko Mizpa nchini Moabu. Akamwambia mfalme wa Moabu, “Nakuomba, baba yangu na mama yangu wakae hapa kwako mpaka nijue Mungu atanifanyia nini.” Basi, Daudi aliwaacha wazazi wake wakae na mfalme wa Moabu; nao wakakaa kwake muda wote ambao Daudi alikuwa ngomeni. Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae hapa ngomeni, ondoka mara moja uende katika nchi ya Yuda.” Basi, Daudi akaondoka, akaenda kwenye msitu wa Herethi. Siku moja, Shauli alikuwa Gibea, amekaa chini ya mkwaju, mlimani, huku akiwa na mkuki wake mkononi na watumishi wake walikuwa wamesimama kandokando yake. Basi akaambiwa kwamba Daudi na watu wake wameonekana. Naye Shauli akawaambia watumishi wake, “Sasa nyinyi watu wa kabila la Benyamini nisikilizeni, je, mnadhani huyu Daudi mwana wa Yese atampa kila mmoja wenu mashamba na mashamba ya mizabibu? Au je, mnadhani atamfamya kila mmoja wenu kamanda wa maelfu au kamanda wa mamia ya majeshi? Kwa nini nyinyi nyote mmekula njama dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu anayeniambia habari hii, wakati mwanangu afanyapo mapatano na mtoto wa Yese. Tena, kwa nini hakuna hata mmoja kati yenu anayesikitika au kunieleza kuwa mwanangu mwenyewe anamchochea mtumishi wangu dhidi yangu akinivizia kama ilivyo leo hii?” Ndipo Doegi, Mwedomu, ambaye alikuwa amesimama karibu na watumishi wa Shauli akasema, “Nilimwona mwana wa Yese akija Nobu kwa kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu. Ahimeleki alimwombea Daudi kwa Mwenyezi-Mungu, akampa chakula na upanga wa yule Mfilisti Goliathi.” Mfalme Shauli akaagiza kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu, pamoja na watu wote wa jamaa ya baba yake ambao walikuwa makuhani huko Nobu waitwe. Wote wakamwendea mfalme Shauli. Shauli akasema, “Sasa sikiliza wewe mwana wa Ahitubu.” Ahimeleki akamjibu, “Naam, bwana.” Shauli akamwambia, “Kwa nini wewe na Daudi mwana wa Yese, mmekula njama dhidi yangu? Kwa nini ulimpatia mikate na upanga, halafu ukamwombea kwa Mungu? Kwa sababu hiyo, leo ameniasi na ananivizia.” Ahimeleki akamjibu, “Kati ya watumishi wako, Daudi ndiye ofisa wa kuaminika kuliko wote. Yeye ni mkwe wako wewe mfalme mwenyewe, kapteni wa kikosi chako cha ulinzi na anaheshimika kuliko wote nyumbani mwako. Leo, sio mara ya kwanza kumwomba Mungu shauri kwa ajili yake. Mfalme, usinishuku mimi wala mtu yeyote katika jamaa ya baba yangu juu ya njama hizo. Mimi mtumishi wako, sijui lolote, liwe kubwa au dogo juu ya jambo hilo.” Lakini mfalme Shauli akamwambia, “Ahimeleki, hakika utauawa, wewe na jamaa yote ya baba yako.” Shauli akawaambia walinzi waliokuwa wamesimama kandokando yake, “Geukeni na kuwaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu, maana wao wanapatana na Daudi; walijua kuwa ametukimbia wala hawakuniarifu.” Lakini walinzi hao hawakuinua mikono yao ili kuwaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu. Kwa hiyo, mfalme Shauli akamwambia Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Doegi, Mwedomu, akaenda na kuwaua makuhani wote. Siku hiyo, Doegi aliua makuhani themanini na watano ambao huvaa vizibao vya kikuhani vya kitani. Kisha aliwaua kwa makali ya upanga wakazi wote wa Nobu, mji wa makuhani, wanaume na wanawake, watoto wadogo na wanyonyao, ng'ombe, punda na kondoo. Lakini Abiathari, mmoja wa watoto wa kiume wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, aliponyoka akakimbilia kwa Daudi. Abiathari alimweleza Daudi kuwa Shauli amewaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu. Naye Daudi akamwambia Abiathari, “Nilijua wazi siku ile nilipomwona Doegi Mwedomu, kuwa atamwambia Shauli. Hivyo, mimi nimesababisha vifo vya watu wa jamaa ya baba yako. Wewe, kaa pamoja nami, wala usiogope. Maana, anayetafuta kuyaangamiza maisha yangu anatafuta hata yako pia. Ukiwa pamoja nami, uko salama kabisa.” Kisha Daudi aliambiwa, “Sikiliza, Wafilisti wanaushambulia mji wa Keila na wanapora nafaka kwenye viwanja vya kupuria.” Basi, Daudi akamwomba Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti hawa?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Ndiyo, nenda ukawashambulie Wafilisti na kuuokoa mji wa Keila.” Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Kama tukiwa hapahapa Yuda tunaogopa, itakuwaje basi, tukienda Keila na kuyashambulia majeshi ya Wafilisti?” Daudi akamwomba tena shauri Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Inuka uende Keila kwani nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” Basi, Daudi akaenda Keila pamoja na watu wake, na huko akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na kuteka nyara ng'ombe wengi. Hivyo Daudi aliwaokoa wakazi wa Keila. Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipokimbilia kwa Daudi huko Keila, alikwenda na kizibao cha kuhani. Shauli alipoambiwa kuwa Daudi amekwisha fika Keila, akasema, “Mungu amemtia mikononi mwangu kwani amejifungia mwenyewe kwa kuingia katika mji wenye malango yenye makomeo.” Hivyo, Shauli aliyaita majeshi yaende Keila na kufanya mashambulizi, ili kumzingira Daudi pamoja na watu wake. Daudi aliposikia mipango miovu ya Shauli dhidi yake, akamwambia kuhani Abiathari, “Kilete hapa hicho kizibao cha kuhani.” Kisha Daudi akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa hakika mimi mtumishi wako, nimesikia kwamba Shauli anapanga kuja kuangamiza mji wa Keila kwa sababu yangu. Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli? Je, Shauli atakuja kweli kama nilivyosikia mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakuomba unijibu mimi mtumishi wako.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Shauli atakuja.” Daudi akamwuliza, “Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli, mimi pamoja na watu wangu?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Watakutia mikononi mwake.” Kisha, Daudi na watu wake ambao walikuwa kama 600, waliondoka na kwenda popote walipoweza kwenda. Shauli aliposikia kwamba Daudi amekwisha kimbia kutoka Keila, akaiacha mipango yake yote. Basi, Daudi alibaki ngomeni jangwani, katika nchi ya milima ya mbuga za Zifu. Shauli alimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia Daudi mikononi mwa Shauli. Daudi alijua kuwa Shauli alitaka kuyaangamiza maisha yake. Daudi akawa katika mbuga za Zifu, huko Horeshi. Yonathani mwana wa Shauli alimfuata Daudi huko Horeshi akamtia moyo kwamba Mungu anamlinda. Yonathani alimwambia, “Usiogope, baba yangu Shauli hatakupata. Wewe utakuwa mfalme wa Israeli, mimi nitakuwa wa pili wako. Hata Shauli baba yangu anajua jambo hili.” Hao wote wawili, wakafanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu. Daudi akabaki mjini Horeshi na Yonathani akaenda zake nyumbani. Shauli alipokuwa bado huko Gibea, Wazifu wakamwendea na kumwambia, “Daudi anajificha katika nchi yetu kwenye ngome huko Horeshi, kwenye mlima Hakila, ulio upande wa kusini wa Yeshimoni. Sasa, mfalme, njoo ili utekeleze yaliyomo moyoni mwako, na kwa upande wetu, jukumu letu litakuwa kumtia Daudi mikononi mwako.” Shauli akawajibu, “Nyinyi kweli mnanionea huruma; Mwenyezi-Mungu na awabariki. Nendeni, mkahakikishe tena, mjue mahali anapojificha, na ni nani amemwona mahali hapo; maana nimeambiwa kwamba yeye ni mjanja sana. Chunguzeni kila upande mjue mahali anapojificha, kisha mniletee habari kamili. Halafu nitakwenda pamoja nanyi na ikiwa bado atakuwa yuko huko, basi, mimi nitamsaka miongoni mwa maelfu yote ya watu wa Yuda.” Basi, wakaondoka kwenda Zifu, wakimtangulia Shauli. Wakati huo, Daudi na watu wake walikuwa katika jangwa la Maoni, katika bonde la Araba kusini mwa Yeshimoni. Shauli na watu wake wakaanza kumtafuta Daudi. Lakini Daudi alipoambiwa habari hizo, alikwenda kujificha kwenye miamba, iliyoko katika mbuga za Maoni na kukaa huko. Shauli aliposikia habari hizo, alimfuatilia Daudi huko kwenye mbuga za Maoni. Shauli na watu wake walikuwa upande mmoja wa mlima, na Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima. Daudi alipokuwa anaharakisha kukimbia, Shauli naye alikuwa anamkaribia kumkamata Daudi. Hapo mtu mmoja akamwendea Shauli na kumwambia, “Njoo haraka; Wafilisti wanaishambulia nchi.” Hivyo, Shauli akaacha kumfuatilia Daudi, akaenda kupigana na Wafilisti. Ndio maana mahali hapo pakaitwa “Mwamba wa Matengano.” Daudi aliondoka mahali hapo, akaenda kuishi kwenye ngome ya mji wa Engedi. Shauli aliporudi kutoka kupigana na Wafilisti, aliambiwa kuwa Daudi yuko kwenye mbuga za Engedi. Kisha Shauli aliwachukua askari 3,000 wateule waliokuwa bora zaidi katika nchi yote ya Israeli, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake katika Miamba ya Mbuzimwitu. Shauli alipokuwa anasafiri, alifika kwenye pango moja lililokuwa karibu na zizi la kondoo, akaingia humo pangoni ili kujisaidia. Daudi na watu wake walikuwa wameketi ndani kabisa ya pango hilo. Watu wa Daudi wakamwambia, “Ile siku aliyokuambia Mwenyezi-Mungu kuwa atakuja kumtia adui yako mikononi mwako nawe umtendee utakavyoona inafaa, leo imefika.” Ndipo Daudi alipomwendea Shauli polepole kutoka nyuma, akakata pindo la vazi lake. Daudi akaanza kufadhaika moyoni kwa sababu alikata pindo la vazi la Shauli kwa siri. Akawaambia watu wake, “Mwenyezi-Mungu anizuie nisimtendee kitendo kama hiki bwana wangu aliyepakwa mafuta na Mwenyezi-Mungu. Nisiunyoshe mkono wangu dhidi ya mtu ambaye Mwenyezi-Mungu amempaka mafuta.” Kwa maneno hayo, Daudi akawashawishi watu wake wasimdhuru Shauli; aliwakataza wasimshambulie. Kisha Shauli akasimama, akatoka pangoni akaendelea na safari yake. Baadaye, Daudi naye akainuka, akatoka pangoni na kumwita Shauli, “Bwana wangu mfalme!” Mfalme Shauli alipoangalia nyuma, Daudi aliinama hadi chini, akamsujudia Shauli. Kisha akamwambia, “Kwa nini unawasikiliza watu wanaokuambia, ‘Angalia! Daudi anataka kukudhuru?’ Sasa tazama, leo umejionea kwa macho yako mwenyewe; ulipokuwa pangoni Mwenyezi-Mungu alikutia mikononi mwangu. Baadhi ya watu wangu waliniambia nikuue, lakini nilikuhurumia. Nikasema sitanyosha mkono wangu dhidi ya bwana wangu kwani yeye ameteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta. Tazama, baba yangu, angalia pindo hili la vazi lako mikononi mwangu; kwa kulikata pindo la vazi lako bila kukuua, unaweza sasa kujua kwa hakika kwamba mimi si mwovu wala mhaini. Mimi sijatenda dhambi dhidi yako ingawa wewe unaniwinda uniue. Mwenyezi-Mungu na aamue kati yangu, na wewe. Yeye akulipize kisasi lakini mimi kamwe sitanyosha mkono wangu dhidi yako. Kumbuka methali ya kale isemayo, ‘Kwa muovu hutoka uovu’; lakini sitanyosha mkono dhidi yako. Sasa wewe mfalme wa Israeli angalia mtu unayetaka kumwua! Je, unamfuatilia nani? Unamfuatilia mbwa mfu! Unakifuatilia kiroboto! Basi, Mwenyezi-Mungu na awe mwamuzi kati yangu na wewe. Yeye na aliangalie jambo hili, anitetee na kuniokoa mikononi mwako.” Daudi alipomaliza kusema, Shauli akasema, “Je, hiyo ni sauti yako mwanangu Daudi?” Shauli akalia kwa sauti. Kisha akamwambia Daudi, “Wewe una haki kuliko mimi; umenilipa mema, hali mimi nimekulipa maovu. Leo, umeonesha jinsi ulivyo mwema kwangu. Hukuniua ijapokuwa Mwenyezi-Mungu alinitia mikononi mwako. Je, mtu akimkamata adui yake atamwacha aende salama? Kwa lile ulilonitendea, Mwenyezi-Mungu na akupe tuzo jema! Sasa nimejua ya kwamba hakika utakuwa mfalme wa Israeli, na ufalme wa Israeli utaimarishwa chini yako. Lakini niapie kwa jina la Mwenyezi-Mungu kuwa hutawakatilia mbali wazawa wangu, wala kufutilia mbali jina langu katika jamaa ya baba yangu.” Daudi akamwapia Shauli. Kisha Shauli akarudi nyumbani kwake, lakini Daudi na watu wake wakaenda kwenye ngome. Sasa, Samueli alifariki; nao Waisraeli wote wakakusanyika ili kumwombolezea. Wakamzika nyumbani kwake huko Rama. Kisha Daudi akaenda zake kwenye nyika za Parani. Kulikuwa na mtu mmoja huko mjini Maoni ambaye alikuwa na biashara ya kondoo mjini Karmeli. Huko Karmeli alifuga kondoo wake na kuwakata manyoya. Alikuwa tajiri sana. Alikuwa na kondoo 3,000 na mbuzi 1,000. Mtu huyo aliitwa Nabali na mkewe aliitwa Abigaili. Abigaili alikuwa mwanamke mwenye akili na mzuri. Lakini Nabali alikuwa mtu wa chuki na duni; tena alikuwa wa ukoo wa Kalebu. Basi, Daudi akiwa huko nyikani alisikia kwamba Nabali alikuwa anawakata kondoo wake manyoya huko Karmeli. Hivyo, akawatuma vijana kumi, akawaambia, “Nendeni kwa Nabali huko Karmeli mkampelekee salamu zangu. Mtamwambia kwamba Daudi anakusalimu hivi: ‘Amani iwe kwako, kwa jamaa yako na yote uliyo nayo. Nimesikia kwamba unawakata manyoya kondoo wako nataka ujue kwamba wachungaji wako walikuwa pamoja nasi, nasi hatukuwadhuru. Tena muda wote walipokuwa pamoja nasi mjini Karmeli, hawakukosa chochote. Ukiwauliza, watakuambia. Sasa nakuomba vijana wangu hawa wapate kibali mbele yako, kwani tumefika wakati wa sikukuu. Tafadhali uwapatie chochote ulicho nacho watumishi wako hawa nami mwanao Daudi.’” Wale vijana wa Daudi walikwenda na kumwambia Nabali kama walivyoagizwa na Daudi. Halafu wakasubiri kidogo. Kisha Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Daudi ni nani? Mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumishi wengi wanaowakimbia mabwana zao. Je, nichukue mikate yangu, maji yangu na nyama niliyowachinjia wakata-manyoya ya kondoo wangu na kuwapa watu ambao sijui hata wanakotoka?” Basi, wale vijana wa Daudi walirudi na kumwambia Daudi walivyojibiwa. Hivyo Daudi akawaambia watu wake, “Kila mtu na ajifunge upanga wake kiunoni.” Kila mtu akajifunga upanga wake, na Daudi pia akajifunga upanga wake; watu wapatao 400 wakamfuata Daudi na watu 200 wakabaki na mizigo. Kijana mmoja wa Nabali, akamwambia Abigaili, mkewe Nabali, “Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani ili kumsalimu bwana wetu. Lakini yeye aliwatukana. Lakini watu hao walikuwa wema sana kwetu, hawakutudhuru; na wakati wote tulipokuwa nao huko nyikani hatukukosa chochote. Kwetu, walikuwa kama ukuta wa ulinzi usiku na mchana muda wote tulipokuwa tunawachunga kondoo. Sasa fikiria juu ya jambo hili na uamue la kufanya. Jambo hili laweza kuleta madhara kwa bwana wetu na jamaa yake yote. Yeye ni mtu mbaya na hakuna anayeweza kuzungumza naye.” Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate 200, viriba viwili vya divai, kondoo watano walioandaliwa vizuri, kilo kumi na saba za bisi, vishada 100 vya zabibu kavu, mikate ya tini 200, na vitu hivi vyote akavipakia juu ya punda. Akamwambia yule kijana wake, “Tangulia! Mimi nitakufuata.” Lakini hakumwambia mumewe lolote. Alipokuwa anateremka, amepanda punda wake, na kukingwa na mlima upande mmoja, akakutana kwa ghafla na Daudi na watu wake wakiwa wanaelekea upande anakotoka. Daudi alikuwa akifikiri, “Mimi nimekuwa nikilinda mali yote ya Nabali nyikani bila faida yoyote na hakuna kitu chake chochote kilichopotea, naye amenilipa mabaya kwa mema niliyomtendea. Mungu na aniue mimi ikiwa kesho asubuhi nitakuwa sijawaua wanaume wake wote.” Abigaili alipomwona tu Daudi, akashuka mara moja kutoka juu ya punda wake, na kuinama mbele ya Daudi hadi uso wake ukagusa chini. Alijitupa miguuni pa Daudi na kumwambia, “Bwana wangu, hatia yote na iwe juu yangu tu. Nakuomba niongee nawe mimi mtumishi wako. Nakuomba usikilize maneno ya mtumishi wako. Usimfikirie Nabali ambaye ni mtu mbaya kwani lilivyo jina lake Nabali, ndivyo naye alivyo. Yeye anaitwa Nabali; na kweli yeye ni mtu mpumbavu. Bwana wangu, wale vijana wako ulipowatuma, mimi mtumishi wako sikuwaona. Sasa bwana wangu, naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, na vile ulivyo hai, kwamba kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekuzuia usilipize kisasi kwa kumwaga damu na kujipatia lawama, waache adui zako na wale wote wanaokutakia mabaya wawe wapumbavu kama Nabali. Bwana wangu, nakuomba upokee zawadi hii niliyokuletea, na uwape vijana wanaokufuata. Nakuomba unisamehe mimi mtumishi wako. Mwenyezi-Mungu atakupa jamaa imara kwa sababu, wewe bwana wangu, unapigana vita vya Mwenyezi-Mungu. Wakati wote wa maisha yako usipatikane na baa lolote. Kukitokea watu wakikufuatilia na kutaka kuyaangamiza maisha yako, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atayasalimisha maisha yako pamoja na walio hai. Lakini maisha ya adui zako atayatupilia mbali, kama vile mtu atupavyo jiwe kwa kombeo. Baada ya Mwenyezi-Mungu kukutendea mema yote aliyokuahidi, na kukuteua kuwa mtawala wa Israeli, wewe bwana wangu, hutakuwa na sababu ya kujuta wala kuhukumiwa na dhamiri kutokana na kumwaga damu bila sababu kwa kujilipiza kisasi. Lakini, bwana wangu, Mwenyezi-Mungu atakapokuwa amekutendea wema huo, nakuomba unikumbuke mimi mtumishi wako.” Daudi akamwambia Abigaili, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliyekutuma leo kukutana nami. Mtukuze Mwenyezi-Mungu aliyekupa busara kwa kunizuia kuwa na hatia ya umwagaji damu na kujilipiza kisasi mimi mwenyewe. Kwa hakika, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, amenizuia nisikudhuru. Usingefanya haraka kuja kukutana nami, kwa hakika, kesho asubuhi hakuna mwanamume yeyote wa Nabali angesalia.” Kisha, Daudi akapokea vitu vyote ambavyo Abigaili alikuwa amemletea, akamwambia Abigaili, “Rudi nyumbani kwako kwa amani. Tazama, mimi nimeyasikia uliyoyasema, na ombi lako nimelipokea.” Abigaili aliporudi nyumbani, alimkuta Nabali akifanya karamu kubwa nyumbani kwake kama ya kifalme. Nabali alikuwa ameburudika sana moyoni kwani alikuwa amelewa sana. Hivyo hakumwambia lolote mpaka asubuhi. Asubuhi, Abigaili alipoona mumewe divai imemtoka, alimweleza mambo yote, na papo hapo Nabali akapooza, akawa kama jiwe. Siku kumi baadaye, Mwenyezi-Mungu alimpiga Nabali akafa. Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, alisema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amemlipiza kisasi Nabali kwa kunitukana, naye Mwenyezi-Mungu ameniepusha mimi mtumishi wake kutenda maovu. Mwenyezi-Mungu amempatiliza Nabali kwa uovu wake.” Kisha Daudi alituma watu ili wamposee Abigaili awe mke wake. Watumishi wa Daudi walipowasili kwa Abigaili huko Karmeli, wakamwambia, “Daudi ametutuma kukuchukua ili uwe mke wake.” Abigaili aliinuka, na kuinama mbele yao mpaka chini, akasema, “Mimi ni mtumishi tu; niko tayari kuosha miguu ya watumishi wa bwana wangu.” Abigaili alifanya haraka, akainuka na kupanda juu ya punda wake, akifuatana na watumishi wake wa kike watano, akaenda na watumishi wa Daudi; naye akawa mke wa Daudi. Tena Daudi alimwoa Ahinoamu kutoka Yezreeli. Hivyo hao wawili wakawa wake zake. Wakati huo, Shauli alikuwa amemwoza binti yake Mikali, ambaye alikuwa mke wa Daudi, kwa Palti mwana wa Laishi, kutoka mji wa Galimu. Baadhi ya wanaume kutoka mji wa Zifu walimwendea Shauli huko Gibea wakamwambia kwamba Daudi alikuwa anajificha kwenye mlima Hakila, upande wa mashariki wa Yeshimoni. Mara moja, Shauli alikwenda kwenye nyika za Zifu kumtafuta Daudi akiwa na askari waliochaguliwa 3,000 wa Israeli. Shauli akapiga kambi juu ya mlima Hakila, karibu na barabara, mashariki ya Yeshimoni. Lakini Daudi alikuwa bado huko nyikani. Daudi alipojua kwamba Shauli alikuwa amekuja nyikani kumtafuta, alituma wapelelezi, akafahamishwa kwamba ni kweli. Daudi akatoka, akaenda mahali Shauli alipopiga kambi. Akapaona mahali ambapo Shauli alikuwa amelala na Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli, alikuwa amelala karibu na Shauli. Shauli alikuwa amelala katikati ya kambi huku akizungukwa na jeshi lake. Daudi akamwambia Ahimeleki ambaye alikuwa, Mhiti, na Abishai ndugu yake Yoabu (mama yao aliitwa Seruya), “Nani atakwenda pamoja nami kwenye kambi ya Shauli?” Abishai akamwambia; “Mimi nitakwenda pamoja nawe.” Hivyo usiku, Daudi na Abishai wakaingia kwenye kambi ya Shauli, wakamkuta Shauli amelala katikati ya kambi hiyo, na mkuki wake umechomekwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri pamoja na askari walikuwa wamelala kumzunguka Shauli. Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Basi, niache nimbane udongoni kwa pigo moja tu la mkuki; sitampiga mara mbili.” Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; maana hakika Mwenyezi-Mungu atamwadhibu mtu yeyote atakayeunyosha mkono wake dhidi ya mteule wake aliyepakwa mafuta. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba Mwenyezi-Mungu mwenyewe atamuua Sauli; ama siku yake ya kufa itafika, au atakwenda vitani na kufia huko. Lakini Mwenyezi-Mungu anakataza nisinyoshe mkono wangu dhidi ya mtu ambaye amemteua kwa kumpaka mafuta. Lakini chukua mkuki wake ulio karibu na kichwa chake pamoja na gudulia lake la maji, halafu tujiendee zetu.” Hivyo, Daudi alichukua ule mkuki na gudulia la maji karibu na kichwa cha Shauli nao wakajiendea zao. Lakini hakuna mtu aliyeona au kujua tukio hilo, wala hakuna aliyeamka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu aliwaletea usingizi mzito. Kisha, Daudi akaenda upande wa pili wa bonde hilo, akasimama juu mlimani mbali na kundi la Shauli. Akaliita kwa sauti jeshi la Shauli na Abneri mwana wa Neri akisema, “Abneri, je, unanisikia?” Abneri akauliza, “Ni nani wewe unayemwita mfalme?” Daudi akamjibu, “Je, wewe si mwanamume? Nani aliye sawa nawe katika Israeli? Mbona basi, hukumlinda bwana wako mfalme? Mtu mmoja wetu aliingia hapo kumwangamiza bwana wako mfalme! Ulilotenda si jambo jema. Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba unastahili kufa, kwa kuwa hukumlinda bwana wako, ambaye Mwenyezi-Mungu amempaka mafuta. Sasa hebu angalia, mkuki wa mfalme na lile gudulia la maji lililokuwa karibu na kichwa chake kama vipo!” Shauli alitambua sauti ya Daudi, akamwuliza, “Je, hiyo ni sauti yako mwanangu Daudi?” Daudi akamjibu, “Bwana wangu, mfalme, ni sauti yangu.” Halafu akaendelea kusema, “Lakini kwa nini, wewe bwana wangu unifuatilie mimi mtumishi wako? Nimefanya nini? Ni ovu gani nimekufanyia? Basi, sasa bwana wangu mfalme, usikie maneno ya mtumishi wako. Ikiwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyekuchochea uje dhidi yangu, basi, na apokee tambiko itakayomfanya abadili nia yake. Lakini kama ni watu, basi, Mwenyezi-Mungu na awalaani watu hao kwani wamenifukuza kutoka urithi aliotupa Mwenyezi-Mungu wakisema, ‘Nenda ukaitumikie miungu mingine.’ Usiniache nife katika nchi ya kigeni, mbali na Mwenyezi-Mungu. Kwa nini wewe mfalme wa Israeli umetoka kuyatafuta maisha yangu kama mtu anayewinda kware milimani?” Ndipo Shauli akajibu, “Mimi nimefanya makosa. Rudi mwanangu Daudi. Sitakudhuru tena kwa kuwa leo maisha yangu yalikuwa ya thamani mbele yako. Mimi nimekuwa mpumbavu na nimekosa vibaya sana.” Daudi akajibu, “Ee mfalme, mkuki wako uko hapa, mtume kijana wako mmoja aje auchukue. Mwenyezi-Mungu humtunza kila mtu kwa uadilifu na uaminifu wake. Leo Mwenyezi-Mungu alikutia mikononi mwangu, lakini mimi sikunyosha mkono wangu dhidi yako kwa kuwa wewe umeteuliwa naye kwa kutiwa mafuta. Tazama kama vile leo maisha yako yalivyokuwa na thamani mbele yangu, ndivyo na maisha yangu yawe na thamani mbele ya Mwenyezi-Mungu; naye akaniokoe kutoka kwenye taabu zote.” Shauli akamwambia Daudi, “Mungu na akubariki mwanangu Daudi. Utafanya mambo makuu, nawe utafanikiwa katika yote.” Basi, Daudi akaenda zake; Shauli naye akarudi nyumbani kwake. Daudi akajisemea moyoni, “Siku moja, Shauli ataniangamiza. Jambo jema kwangu ni kukimbilia katika nchi ya Wafilisti. Shauli atakata tamaa kunitafuta ndani ya mipaka ya nchi ya Israeli, nami nitakuwa salama kutoka mikononi mwake.” Hivyo, mara moja Daudi na watu wake 600 wakaenda kwa Akishi mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi. Daudi na watu wake pamoja na jamaa yake wakaishi na Akishi huko Gathi. Daudi alikuwa na wake wawili: Ahinoamu kutoka Yezreeli na Abigaili mjane wa Nabali kutoka mji wa Karmeli. Shauli aliposikia kwamba Daudi amekimbilia Gathi, hakumfuata tena. Siku moja, Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali mbele yako nakuomba unipe mji mmoja nchini mwako ili uwe mahali pangu pa kuishi. Hakuna haja kwangu kuishi nawe katika mji huu wa kifalme.” Siku hiyo, Akishi akampa mji wa Siklagi. Hivyo, tangu siku hiyo mji wa Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda. Daudi aliishi katika nchi ya Wafilisti kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne. Katika muda huo, Daudi na watu wake waliwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki, ambao walikuwa wenyeji wa nchi hiyo tangu zamani. Aliwashambulia katika nchi yao mpaka Shuri, mpakani na Misri. Daudi aliipiga nchi hiyo asimwache hai mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, akateka kondoo, ng'ombe, punda, ngamia na mavazi; kisha akarudi na kufika kwa Akishi. Akishi alipomwuliza, “Leo mashambulizi yako yalikuwa dhidi ya nani?” Daudi alimwambia, “Dhidi ya Negebu ya Yuda” au “Dhidi ya Negebu ya Wayerameeli” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni.” Daudi hakumwacha mtu yeyote hai awe mwanamume au mwanamke ili aletwe Gathi; alifikiri moyoni: “Wanaweza wakaeleza juu yetu na kusema, ‘Daudi alifanya kitendo hiki na kile.’” Hivyo ndivyo Daudi alivyozoea kutenda wakati wote alipoishi katika nchi ya Wafilisti. Kwa hiyo, Akishi alimsadiki Daudi, akifikiri, “Wananchi wenzake Waisraeli hawampendi kabisa; kwa hiyo, atanitumikia maisha yake yote.” Baada ya muda fulani, Wafilisti walikusanya majeshi yao tayari kwenda kupigana na Waisraeli. Akishi akamwambia Daudi, “Uelewe vizuri kwamba wewe na watu wako mnapaswa kwenda pamoja nami kupigana vita.” Daudi akamjibu Akishi, “Naam! Utaona kitu ambacho mtumishi wako anaweza kufanya.” Akishi akamwambia, “Nami nitakufanya kuwa mlinzi wangu binafsi wa maisha.” Wakati huu, Samueli alikuwa amekwisha fariki, na Waisraeli wote walikuwa wamekwisha mwombolezea na kumzika katika mji wake Rama. Shauli alikuwa amewafukuza kutoka nchini watabiri na wachawi. Wafilisti walikusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu; na Shauli aliwakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao kwenye mlima Gilboa. Shauli alipoona jeshi la Wafilisti alianza kuogopa, akaanza kutetemeka kwa hofu aliyokuwa nayo moyoni mwake. Hata alipomwomba Mwenyezi-Mungu shauri, Mwenyezi-Mungu hakumjibu kwa ndoto, kwa mawe ya kauli, wala kwa njia ya manabii. Ndipo Shauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke ambaye anaweza kutabiri ili nimwendee na kumtaka shauri.” Watumishi wake wakamjibu, “Yuko mtabiri mmoja huko Endori.” Basi, Shauli akajigeuza na kuvaa mavazi mengine, akaenda huko pamoja na watu wake wawili. Walifika kwa huyo mwanamke usiku, akamwambia, “Nitabirie kwa pepo, umlete duniani yeyote nitakayekutajia.” Yule mwanamke akamwambia, “Wewe unajua kwa hakika kuwa mfalme Shauli amewaangamiza kabisa watabiri na wachawi wote katika nchi ya Israeli. Sasa kwa nini unaniwekea mtego wa kuninasa na kuniua?” Shauli akamwapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akisema, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba hakuna adhabu yoyote itakayokupata kutokana na jambo hili.” Yule mwanamke akamwuliza, “Je, nikuletee nani kutoka huko?” Shauli akajibu, “Niletee Samueli.” Yule mwanamke alipomwona Samueli alilia kwa sauti kuu, akamwambia Shauli, “Kwa nini umenidanganya? Wewe ni Shauli!” Mfalme Shauli akamwambia, “Usiogope! Unaona nini?” Yule mwanamke akamjibu, “Naona mungu akitokea ardhini.” Shauli akamwambia mwanamke, “Ni mfano wa nani?” Yule mwanamke akamwambia, “Mwanamume mzee anapanda juu, naye amejizungushia joho.” Hapo, Shauli akatambua kwamba huyo ni Samueli. Shauli akainama hadi chini, na kusujudu. Samueli akamwambia Shauli, “Kwa nini unanisumbua kwa kunileta juu?” Shauli akamjibu, “Mimi nina taabu kubwa! Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, na Mungu amenipa kisogo; hanijibu tena kwa njia ya manabii wala kwa ndoto. Ndio maana nimekuita unijulishe la kufanya.” Samueli akasema, “Kwa nini unaniomba shauri ambapo Mwenyezi-Mungu amekupa kisogo na amekuwa adui yako? Mwenyezi-Mungu amekutendea kile alichokuambia kwa njia yangu. Mwenyezi-Mungu ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, na amempa Daudi jirani yako. Maana, wewe hukuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, wala hukuitekeleza ghadhabu yake dhidi ya Waamaleki. Ndio maana leo Mwenyezi-Mungu amekutendea mambo haya. Zaidi ya hayo, Mwenyezi-Mungu atakutia wewe pamoja na Waisraeli wote mikononi mwa Wafilisti. Kesho, wewe na wanao mtakuwa pamoja nami; hata jeshi la Israeli Mwenyezi-Mungu atalitia mikononi mwa Wafilisti.” Ghafla, Shauli akiwa na hofu kutokana na maneno ya Samueli, alianguka kifudifudi; hakuwa na nguvu zozote; kwa kuwa alikuwa hajala chochote kwa siku nzima, usiku na mchana. Ndipo yule mwanamke alipomwendea Shauli, na alipoona kuwa Shauli ameshikwa na hofu mno, alimwambia, “Mimi mtumishi wako nimehatarisha maisha yangu kwa kufanya kile ulichoniambia nikufanyie. Sasa, nisikilize mimi mtumishi wako; nitakuandalia mkate ili ule nawe utakuwa na nguvu za kuendelea na safari yako.” Lakini Shauli alikataa na kusema, “Sitakula.” Lakini watumishi pamoja na yule mwanamke, walimsihi ale, naye akawasikiliza. Hivyo aliinuka kutoka chini na kukaa kwenye kitanda. Yule mwanamke alikuwa na ndama wake mmoja nyumbani aliyenona, akamchinja haraka, akachukua unga wa ngano, akaukanda, akatengeneza mkate usiotiwa chachu. Akampa Shauli, akawapa pia watumishi wake, nao wakala. Halafu wakaondoka na kwenda zao wakati huohuo usiku. Wafilisti walikusanya majeshi yao yote huko Afeka, na Waisraeli walipiga kambi kwenye chemchemi ya bonde la Yezreeli. Wakuu watano wa Wafilisti walipokuwa wakipita na vikosi vyao vya mamia na maelfu, Daudi naye akiwa na watu wake pamoja na Akishi walikuwa wanafuata upande wa nyuma wa jeshi hilo. Makamanda wa Wafilisti waliuliza, “Waebrania hawa wanafanya nini hapa?” Akishi akawajibu hao makamanda Wafilisti, “Huyu ni Daudi, mtumishi wa Shauli mfalme wa Israeli; naye amekuwa nami kwa muda mrefu: Miaka kadhaa. Na tangu alipokimbilia kwangu, sijampata na kosa lolote.” Lakini makamanda wa Wafilisti walimkasirikia sana Akishi, wakamwambia, “Mrudishe aende mahali ulikompa akae. Kamwe asiende pamoja nasi vitani, la sivyo wakati wa vita atageuka na kuwa adui yetu. Huoni kuwa mtu huyu atapata njia nzuri ya kupatana na bwana wake halafu kuwa adui yetu vitani? Je, huyu si Daudi yuleyule ambaye wanawake waliimba habari zake walipokuwa wakicheza, ‘Shauli ameua maelfu, lakini Daudi ameua maelfu kumi.’” Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba umekuwa mwaminifu kwangu. Lingekuwa jambo jema kwangu twende wote vitani, kwa maana sijaona lolote baya kwako tangu siku ile ulipokuja kwangu hadi leo hii. Hata hivyo, wakuu hawajaridhika nawe. Hivyo sasa, rudi nyumbani. Nenda kwa amani ili usiwachukize wakuu wa Wafilisti.” Daudi akamwambia Akishi, “Lakini nimefanya nini? Kama unavyosema kuwa, hujaniona na kosa lolote tangu siku ile nilipoanza kukutumikia hadi leo, kwa nini nisiende kupigana na maadui za bwana wangu, mfalme?” Akishi akamwambia, “Najua kuwa huna lawama mbele yangu kama malaika wa Mungu. Hata hivyo, makamanda wa Wafilisti wamesema, ‘Kamwe asiende pamoja nasi vitani’. Sasa, wewe pamoja na watumishi wa bwana wako Shauli waliokuja pamoja nawe, kesho asubuhi na mapema, amkeni na kuondoka mara kunapopambazuka.” Hivyo, kesho yake asubuhi, Daudi pamoja na watu wake waliondoka kurudi katika nchi ya Wafilisti. Lakini hao Wafilisti wakaenda Yezreeli. Siku ya tatu baadaye, Daudi na watu wake wakarudi Siklagi. Waamaleki walikuwa wamekwisha shambulia Negebu pamoja na mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto. Walikuwa wameteka wanawake na watu wote waliokuwa mjini humo, wakubwa kwa wadogo. Hao waliowateka, waliondoka nao wakiwa hai, bila ya kumwua mtu yeyote. Daudi na watu wake walipofika mjini waliukuta mji umeteketezwa, na wanawake, watoto wao wa kiume na wa kike, wamechukuliwa mateka. Ndipo Daudi na watu wake walipoangua kilio, wakalia hadi walipoishiwa nguvu. Wake wawili wa Daudi, Ahinoamu kutoka Yezreeli na Abigaili mjane wa Nabali, nao pia walikuwa wamechukuliwa mateka. Sasa, Daudi alikuwa katika matatizo makubwa kwa kuwa watu wake walikuwa na uchungu rohoni mwao kwa kupoteza watoto wao; hivyo wakawa wanamtishia kumpiga mawe. Lakini Daudi alijipa moyo kwa kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kizibao cha kuhani.” Abiathari akampelekea. Daudi akamwomba Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, genge hili nilifuate? Na je nitalikamata?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Lifuate kwani utalipata na kuwaokoa hao waliotekwa.” Kwa hiyo, Daudi akaondoka pamoja na wale watu 600 aliokuwa nao. Walipofika kwenye kijito cha Besori, wakawakuta baadhi ya watu waliotekwa wameachwa hapo. Lakini Daudi aliendelea kulifuatilia lile genge akiwa na watu 400, watu 200 wakabaki hapo kwani walichoka mno, wasiweze kuvuka kijito hicho. Wale watu waliokuwa na Daudi walimkuta mtu mmoja Mmisri nyikani, nao wakampeleka kwa Daudi. Wakampa mtu huyo mkate na maji. Pia walimpa kipande cha mkate wa tini na vishada viwili vya zabibu kavu. Alipomaliza kula, akapata nguvu, kwani alikuwa hajala wala kunywa kitu chochote kwa muda wa siku tatu, mchana na usiku. Daudi akamwuliza, “Bwana wako ni nani? Na umetoka wapi?” Yeye akamwambia, “Mimi ni kijana Mmisri. Ni mtumishi wa Mmaleki mmoja. Bwana wangu aliniacha nyuma siku tatu zilizopita kwa kuwa nilikuwa mgonjwa. Sisi tulishambulia sehemu ya jangwa wanamoishi Wakerethi, eneo la Yuda pamoja na sehemu ya jangwa unakoishi ukoo wa Kalebu, tukauteketeza kwa moto mji wa Siklagi.” Daudi akamwuliza, “Je, utaweza kunipeleka kwenye genge hilo?” Kijana akamjibu, “Ikiwa utaniapia kwa jina la Mungu kuwa hutaniua, wala kunitia mikononi mwa bwana wangu, nitakupeleka.” Yule kijana alimwongoza Daudi hadi genge lile lilipokuwa. Walipofika huko waliwakuta wateka nyara hao wakiwa wametawanyika kila mahali kwani walikuwa wakila na kunywa kwa sababu nyara walizoteka kutoka nchi ya Wafilisti na nchi ya Yuda zilikuwa nyingi sana. Daudi aliwapiga tangu asubuhi hadi siku ya pili jioni. Hakuna mwanamume yeyote aliyenusurika isipokuwa vijana 400 ambao walipanda ngamia na kukimbia. Daudi aliokoa kila kitu Waamaleki walichokuwa wamekiteka, hata na wake zake wawili. Chochote kilichokuwa chao, kiwe kikubwa au kidogo, mtoto wa kiume au wa kike, Daudi alikikomboa. Pia Daudi aliyarudisha makundi yote ya kondoo na ng'ombe, na watu wake wakawa wanaswaga wanyama hao wakiwatanguliza mbele ya wanyama wale wengine wakisema, “Nyara za Daudi.” Daudi akawarudia wale watu 200 ambao waliachwa kwenye kijito cha Besori kwa sababu walikuwa wamechoka kumfuata. Wale watu walipomwona Daudi pamoja na wale waliokuwa pamoja naye, wakaenda kumlaki. Daudi alipofika karibu na watu hao, akawasalimu. Lakini watu wote waovu na baradhuli miongoni mwa watu waliofuatana na Daudi, wakasema, “Hatutawapa watu hawa nyara zozote tulizozikomboa kwani hawakwenda pamoja nasi. Ila wawachukue wake zao na watoto wao, waende zao.” Daudi akawaambia, “Sivyo ndugu zangu. Hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambacho Mwenyezi-Mungu ametupa. Alitulinda salama, na akalitia mikononi mwetu genge lililokuja kutushambulia. Hakuna mtu atakayekubaliana na mawazo yenu! Yule aliyekwenda vitani na yule aliyebaki na mizigo yetu, kila mtu atapewa sehemu inayolingana na mwenzake.” Tangu siku hiyo Daudi alifanya uamuzi huo kuwa sheria na kanuni katika nchi ya Israeli hadi hivi leo. Daudi aliporejea Siklagi, aliwapelekea rafiki zake, ambao ni wazee wa Yuda, sehemu ya nyara akisema, “Nawapelekea zawadi kutoka nyara za maadui wa Mwenyezi-Mungu.” Zawadi hizo zilikuwa kwa ajili ya wakazi wa Betheli, wakazi wa Ramothi katika Negebu, wakazi wa Yatiri, wakazi wa Aroeri, wakazi wa Sifmothi, wakazi wa Eshtemoa, wakazi wa Rakali, wakazi wa miji ya Wayerameeli, wakazi wa miji ya Wakeni, wakazi wa Horma, wakazi wa Borashani, wakazi wa Athaki, na wakazi wa Hebroni. Daudi aliwapelekea pia wakazi wa miji yote ambako yeye na watu wake walitembelea. Basi, Wafilisti walipigana vita dhidi ya Waisraeli; nao Waisraeli walikimbia mbele ya Wafilisti, na kuuawa katika mlima wa Gilboa. Lakini Wafilisti wakamzingira Shauli na wanawe, kisha wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-shua, wana wa Shauli. Vita vilikuwa vikali sana dhidi ya Shauli. Wapiga mishale walipomwona walimjeruhi vibaya. Ndipo Shauli alipomwambia mtu aliyembebea silaha, “Chomoa upanga wako unichome nife, ili watu hawa wasiotahiriwa wasije wakanichoma upanga na kunidhihaki.” Lakini huyo aliyembebea silaha hakuthubutu kwa sababu aliogopa sana. Hivyo, Shauli alichukua upanga wake mwenyewe, na kuuangukia. Halafu yule aliyembebea silaha alipoona kuwa Shauli amekufa, naye pia aliuangukia upanga wake, akafa pamoja na Shauli. Hivyo ndivyo Shauli alivyokufa, na wanawe watatu, pia na mtu aliyembebea silaha pamoja na watu wake wote katika siku hiyohiyo moja. Nao Waisraeli waliokuwa upande wa pili wa bonde, na wengine waliokuwa upande wa mashariki wa mto Yordani walipoona kuwa Waisraeli wamekimbia, naye Shauli na wanawe wamekufa, waliihama miji yao, wakakimbia. Wafilisti wakaenda na kukaa katika miji hiyo. Kesho yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa walizikuta maiti za Shauli na wanawe mlimani Gilboa. Walikata kichwa cha Shauli na kumvua silaha zake; halafu waliwatuma wajumbe katika nchi yao yote ya Filistia kutangaza habari njema nyumbani mwa sanamu zao na kwa watu. Zile silaha zake waliziweka nyumbani mwa Maashtarothi; kisha wakautundika mwili wake kwenye ukuta wa mji wa Beth-sheani. Lakini wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi waliposikia Wafilisti walivyomtendea Shauli, mashujaa wote waliondoka, wakasafiri usiku kucha, wakaondoa mwili wa Shauli na miili ya wanawe kutoka ukuta wa Beth-sheani; wakaja nayo mpaka Yabeshi na kuiteketeza huko. Baadaye, wakaichukua mifupa yao na kuizika chini ya mkwaju huko Yabeshi; nao wakafunga kwa muda wa siku saba. Baada ya kifo cha Shauli, Daudi alirudi baada ya kuwashinda Waamaleki, akakaa Siklagi kwa muda wa siku mbili. Siku iliyofuata, mtu mmoja kutoka kambi ya Shauli, mavazi yake yakiwa yamechanwa kwa huzuni na akiwa na mavumbi kichwani alimwendea Daudi. Alipomfikia Daudi, alijitupa chini mbele yake akamsujudia. Daudi akamwambia, “Unatoka wapi?” Naye akamwambia, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.” Daudi akamwambia, “Niambie mambo yalivyokuwa huko.” Yule mtu akamjibu, “Watu wetu wameyakimbia mapigano na wengi wetu wameuawa. Zaidi ya hayo, Shauli na mwanawe Yonathani pia wameuawa.” Daudi akamwuliza yule kijana, “Unajuaje kuwa Shauli na Yonathani mwanawe wamekufa?” Yule kijana akamjibu, “Kwa bahati, nilikuwapo mlimani Gilboa. Nilimwona Shauli ameegemea mkuki wake na magari ya wapandafarasi ya adui zake yalikuwa yanamsonga sana. Shauli alipotazama nyuma, aliniona, akaniita. Nilipoitika, yeye aliniuliza mimi ni nani, nami nikamwambia kuwa mimi ni Mmaleki. Hapo, akaniambia, ‘Karibia uniue maana nimejeruhiwa vibaya na maumivu ni makali. Lakini bado ningali hai’. Hivyo, nilikwenda karibu naye na kumuua, kwa sababu nilikuwa na uhakika kuwa akianguka chini, hataweza kuishi zaidi. Lakini taji iliyokuwa kichwani pake na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, vyote nimekuletea wewe, bwana wangu.” Daudi akayashika mavazi yake na kuyararua kwa huzuni. Hata watu waliokuwa pamoja na Daudi wakafanya vivyo hivyo. Wakaomboleza, wakalia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Shauli, Yonathani mwanawe, na nchi ya Waisraeli, watu wa Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa wengi wao waliuawa vitani. Daudi akamwuliza yule kijana aliyempasha habari, “Unatoka wapi?” Yeye akajibu, “Mimi ni Mmaleki, lakini ninaishi katika nchi yako kama mgeni.” Daudi akamwuliza, “Ilikuwaje wewe hukuogopa kuunyosha mkono wako na kumuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta?” Kisha, Daudi akamwita mmoja wa vijana wake akamwambia, “Muue mtu huyu!” Yule kijana alimpiga yule Mmaleki, naye akafa. Daudi akasema, “Uwajibike wewe mwenyewe kwa kifo chako, maana umejishuhudia wewe mwenyewe kwa mdomo wako ukisema, ‘Nimemuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta.’” Daudi aliimba ombolezo lifuatalo kwa ajili ya Shauli na mwanawe Yonathani. Daudi alisema watu wa Yuda wafundishwe ombolezo hilo, nalo limeandikwa katika kitabu cha Yashari. Daudi aliimba, “Walio fahari yako, ee Israeli, wameuawa milimani pako. Jinsi gani mashujaa walivyoanguka! Jambo hilo msiuambie mji wa Gathi wala katika mitaa ya Ashkeloni. La sivyo, wanawake Wafilisti watashangilia, binti za wasiotahiriwa, watafurahi. “Enyi milima ya Gilboa, msiwe na umande au mvua juu yenu. Wala mashamba yenu daima yasitoe chochote. Maana huko ngao za shujaa zilitiwa najisi, ngao ya Shauli haikupakwa mafuta. “Upinde wa Yonathani kamwe haukurudi nyuma, upanga wa Shauli kamwe haukurudi bure, daima ziliua wengi. Naam, ziliua mashujaa. “Shauli na Yonathani, watu wa ajabu na wakupendeza. Maishani na kifoni hawakutengana. Walikuwa wepesi kuliko tai, naam, wenye nguvu kuliko simba. “Wanawake wa Israeli, mlilieni Shauli! Aliwavika mavazi mekundu ya fahari, aliyatarizi mavazi yenu kwa dhahabu. “Jinsi gani mashujaa walivyoanguka! Wamekufa wakiwa katika mapambano. Yonathani analala, akiwa ameuawa milimani. Nasikitika kwa ajili yako, ndugu yangu Yonathani. Umekuwa kwangu daima mtu wa kupendeza, pendo lako kwangu limekuwa la ajabu, la ajabu kuliko la mwanamke. “Jinsi gani mashujaa wameanguka, na silaha zao zimeachwa, hazina kazi.” Baada ya mambo haya, Daudi alimwomba Mwenyezi-Mungu shauri, akasema, “Je, niende kwenye mji mmojawapo wa miji ya Yuda?” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda!” Daudi akamwuliza, “Niende mji upi?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Nenda kwenye mji wa Hebroni.” Hivyo, Daudi alikwenda Hebroni, pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali, kutoka mji wa Karmeli. Aliwachukua watu wake, kila mtu akiwa pamoja na jamaa yake; nao wakafanya makao yao katika miji iliyokuwa kandokando ya Hebroni. Watu wa Yuda walimwendea Daudi huko Hebroni wakampaka mafuta awe mfalme wao. Daudi aliposikia kuwa watu wa Yabesh-gileadi ndio waliomzika Shauli, aliwatuma watu huko Yabesh-gileadi na ujumbe: “Mwenyezi-Mungu na awabariki kwa maana mlionesha utii wenu kwa Shauli, bwana wenu, kwa kumzika. Sasa, Mwenyezi-Mungu awafadhili na kuwa mwaminifu kwenu. Nami nitawatendea mema kutokana na jambo mlilolitenda. Lakini muwe imara na mashujaa. Shauli, bwana wenu, amekufa, na watu wa Yuda wamenipaka mafuta niwe mfalme wao.” Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli alikuwa amemchukua Ishboshethi mwana wa Shauli na kumpeleka huko Mahanaimu. Huko, Abneri akamtawaza Ishboshethi kuwa mfalme wa nchi ya Gileadi, Ashuru, Yezreeli, Efraimu na Benyamini na Israeli yote. Ishboshethi alikuwa na umri wa miaka arubaini alipoanza kuitawala Israeli, naye alitawala kwa muda wa miaka miwili. Lakini kabila la Yuda lilimfuata Daudi. Daudi alikuwa mfalme wa kabila la Yuda kwa muda wa miaka saba na nusu, makao yake yalikuwa huko Hebroni. Abneri mwana wa Neri, pamoja na maofisa wa Ishboshethi, mwana wa Shauli, waliondoka Mahanaimu na kwenda Gibeoni. Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wengine wa Daudi, nao walitoka na kukutana na Abneri na watu aliokuwa nao kwenye bwawa lililoko huko Gibeoni. Kikosi kimoja upande mmoja wa bwawa na kingine upande mwingine. Abneri akamwambia Yoabu, “Waruhusu vijana wapambane mbele yetu!” Yoabu akamjibu, “Sawa.” Ndipo vijana ishirini na wanne wakatolewa: Upande wa kabila la Benyamini na Ishboshethi mwana wa Shauli, vijana kumi na wawili; na upande wa Daudi vijana kumi na wawili. Kila mmoja alimkamata adui yake kichwani, akamchoma mpinzani wake upanga, hivyo wote wawili wakaanguka chini, wamekufa. Hivyo, mahali hapo pakaitwa Helkath-hazurimu. Mahali hapo pako huko Gibeoni. Vita vya siku hiyo vilikuwa vikali. Abneri na watu wa Israeli walipigwa vibaya na watu wa Daudi. Wana watatu wa Seruya: Yoabu, Abishai na Asaheli walikuwapo hapo. Asaheli alikuwa na mbio kama paa. Asaheli alimfuatia Abneri moja kwa moja bila kugeuka kulia wala kushoto. Abneri alipoangalia nyuma na kumwona Asaheli, alimwambia, “Je, ni wewe Asaheli?” Yeye akamjibu, “Naam, ni mimi.” Abneri akamwambia, “Geukia kulia au kushoto, umkamate kijana mmoja na kuchukua nyara zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfuatia. Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, “Acha kunifuatia. Kwa nini nikuue? Nitawezaje kuonana na kaka yako Yoabu?” Lakini Asaheli alikataa. Hivyo Abneri akampiga mkuki tumboni kinyumenyume, na mkuki huo ukatokeza mgongoni kwa Asaheli. Asaheli akaanguka chini, na kufa papo hapo. Watu wote waliofika mahali alipofia Asaheli, walisimama kimya. Lakini Yoabu na Abishai walimfuatia Abneri. Jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye mlima wa Ama, ulioko mashariki ya Gia, katika barabara iendayo jangwa la Gibeoni. Watu wa kabila la Benyamini wakajikusanya pamoja wakawa nyuma ya Abneri, hivyo wakaunda kikosi chao; nao wakasimama juu ya mlima. Kisha Abneri akamwita Yoabu, “Je, tutapigana siku zote? Je, huoni kwamba mwisho utakuwa mchungu? Je, utaendelea kwa muda gani bila kuwashawishi watu wako waache kuwaandama ndugu zao?” Yoabu akamwambia, “Naapa kwa Mungu aliye hai, kwamba kama hungesema jambo hilo, hakika watu wangu wangeendelea kuwaandama ndugu zao hadi kesho asubuhi.” Hivyo, Yoabu akapiga tarumbeta na watu wakaacha kuwafuatia watu wa Israeli, wala hawakupigana zaidi. Abneri na watu wake walipita bonde la Araba usiku kucha. Wakavuka mto Yordani, wakatembea mchana kutwa hadi Mahanaimu. Yoabu aliporudi kutoka kumfuatia Abneri, aliwakusanya watu wake wote, akagundua kuwa watumishi kumi na tisa wa Daudi walikosekana, licha ya Asaheli. Lakini watumishi wa Daudi walikuwa wamewaua watu 360 kutoka kabila la Benyamini pamoja na watu wa Abneri. Yoabu na watu wake waliuchukua mwili wa Asaheli, wakauzika kwenye kaburi la baba yake, lililoko huko Bethlehemu. Yoabu na watu wake walitembea usiku kucha, na kulipokucha wakafika mjini Hebroni. Kulikuwa na vita vya muda mrefu kati ya watu walioiunga mkono jamaa ya Shauli, na wale walioiunga mkono jamaa ya Daudi. Lakini Daudi alizidi kupata nguvu zaidi na zaidi, ambapo upande wa Shauli ulizidi kudhoofika zaidi na zaidi. Watoto wa kiume aliozaliwa Daudi huko Hebroni walikuwa: Amnoni, mzaliwa wake wa kwanza, mama yake alikuwa Ahinoamu kutoka Yezreeli; Kileabu, mzaliwa wake wa pili, mama yake alikuwa Abigaili, mjane wa Nabali kutoka Karmeli; Absalomu, mzaliwa wake wa tatu, mama yake alikuwa Maaka, bintiye Talmai mfalme wa Geshuri; Adoniya, mzaliwa wake wa nne, mama yake alikuwa Hagithi; Shefatia, mzaliwa wake wa tano, mama yake alikuwa Abitali, na Ithreamu, mzaliwa wake wa sita, mama yake alikuwa Egla, mke wake Daudi. Daudi alizaliwa wana hawa wote alipokuwa huko Hebroni. Kadiri vita vilivyoendelea kati ya jamaa ya Daudi na ile ya Shauli, Abneri alizidi kujiimarisha katika jamaa ya Shauli. Shauli alikuwa na suria mmoja aitwaye Rispa, binti Aya. Basi, wakati mmoja, Ishboshethi akamwuliza Abneri, “Kwa nini umelala na suria wa baba yangu?” Abneri alikasirika sana kutokana na maneno ya Ishboshethi, akasema: “Je, unafikiri mimi naweza kumsaliti Shauli? Je, unafikiri kuwa mimi naitumikia jamaa ya Yuda? Tazama, mimi nimekuwa mtiifu kwa jamaa ya baba yako Shauli, ndugu zake, rafiki zake na sijakutia mikononi mwa Daudi hadi leo. Hata hivyo, leo hii unaniona kuwa mwenye hatia kwa ajili ya mwanamke. Mungu aniue ikiwa sitatekeleza yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi. Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi kuwa atauhamisha ufalme kutoka jamaa ya Shauli na kumpa yeye. Naye atatawala Israeli na Yuda kutoka Dani hadi Beer-sheba.” Ishboshethi hakuweza kusema neno, kwa kuwa alikuwa anamwogopa Abneri. Basi, Abneri akatuma wajumbe kwa Daudi, huko Hebroni wakamwambie, “Je, nchi hii ni mali ya nani? Fanya agano na mimi, nami nitakusaidia kuifanya Israeli yote iwe chini yako.” Daudi akamjibu, “Vema, nitafanya agano nawe. Lakini ninakutaka jambo moja kwamba kabla hujaniona sharti kwanza uniletee Mikali binti wa Shauli. Hapo utaniona.” Daudi pia alituma wajumbe kwa Ishboshethi mwana wa Shauli akisema, “Nirudishie mke wangu Mikali ambaye nilimwoa kwa magovi 100 ya Wafilisti.” Basi, Ishboshethi alituma watu wakamchukue Mikali kutoka kwa mumewe, Paltieli mwana wa Laishi. Lakini Paltieli akaenda pamoja na mkewe huku analia njia nzima mpaka huko Bahurimu. Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani.” Naye akarudi. Abneri alifanya mashauri na wazee wa Israeli, akawaambia, “Kwa muda fulani uliopita mmekuwa mkitaka Daudi awe mfalme wenu. Sasa, lileteni jambo hilo hadharani kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimwahidi hivi Daudi, ‘Kwa mkono wako wewe Daudi mtumishi wangu, nitawaokoa watu wangu wa Israeli kutoka kwa Wafilisti na kutoka kwa adui zao wengine.’” Abneri pia akazungumza na Wabenyamini, kisha akaenda mpaka Hebroni kumwambia Daudi kuhusu yale ambayo watu wote wa Israeli na kabila lote la Benyamini walipatana kutenda. Abneri alipomwendea Daudi, alikuwa na watu ishirini, Daudi aliwafanyia karamu. Abneri akamwambia Daudi, “Mimi sasa nitakwenda na kukuletea watu wote wa Israeli, wewe bwana wangu mfalme. Watakuja na kufanya agano nawe, ili uwe mfalme wao, nawe utawatawala wote kama upendavyo.” Daudi akamuaga Abneri aende zake, naye akaondoka kwa amani. Baadaye, Yoabu na baadhi ya watu wa Daudi walirudi kutoka mashambulio, wakaleta nyara nyingi. Lakini Abneri hakuwa pamoja na Daudi huko Hebroni kwani Daudi alikuwa amemuaga aende zake, naye akaondoka kwa amani. Yoabu aliporudi akiwa na jeshi lake lote alilokuwa nalo, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri, alikuwa amekuja kumwona mfalme Daudi, naye amemuaga aende zake, naye ameondoka kwa amani. Yoabu alimwendea mfalme na kumwambia, “Sasa umefanya nini? Tazama Abneri alikuja kwako, kwa nini umemwacha aende? Je, unajua kuwa Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya? Alikuja ili ajue mienendo yako na yale unayoyafanya.” Yoabu alipotoka kuzungumza na Daudi, alituma wajumbe wakamlete Abneri, nao wakamkuta kwenye kisima cha Sira na kumrudisha, lakini Daudi hakujua jambo hilo. Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu alimchukua kando kwenye lango kana kwamba anataka kuzungumza naye kwa faragha. Hapo Yoabu akamkata Abneri tumboni kwa sababu Abneri alikuwa amemuua Asaheli ndugu yake, na Abneri akafa. Baadaye Daudi aliposikia habari hizo alisema, “Mimi na ufalme wangu hatuna hatia mbele ya Mwenyezi-Mungu kuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri. Lawama ya mauaji hayo yawe juu ya kichwa cha Yoabu na jamaa yote ya baba yake! Jamaa ya Yoabu daima isikose mtu mwenye ugonjwa wa kisonono, au ugonjwa wa ukoma, au anayetembea kwa magogo au kuuawa kwa upanga, au mwenye kukosa chakula!” Yoabu na ndugu yake Abishai walimuua Abneri kwa kuwa alikuwa amemuua ndugu yao Asaheli wakati wa vita huko Gibeoni. Kisha, mfalme Daudi akamwambia Yoabu na wale wote waliokuwa pamoja naye, wararue mavazi yao, wavae mavazi ya gunia ili wamwombolezee Abneri. Wakati wa mazishi hayo, mfalme Daudi alitembea nyuma ya jeneza. Abneri alizikwa huko Hebroni na mfalme aliomboleza kwa sauti akiwa kando ya kaburi, pia watu wengine wote walifanya vivyo hivyo. Mfalme alimwombolezea Abneri akisema, “Je, ilikuwaje Abneri akafa kama mpumbavu? Mikono yako haikufungwa na miguu yako haikutiwa pingu. Amekufa kama mtu aliyeuawa na waovu!” Na watu wote walimlilia tena. Kisha, watu wote walikwenda kumshawishi Daudi ale mkate wakati ulipokuwa bado mchana. Lakini Daudi aliapa akawaambia, “Mungu na aniue ikiwa nitaonja mkate au kitu chochote hadi jua litakapotua.” Watu wote waliyaona mambo hayo, nao walipendezwa; kama vile kila kitu alichofanya mfalme kilivyowapendeza. Hivyo, siku ile, Waisraeli wote walielewa kwamba haikuwa nia ya mfalme Daudi kumuua Abneri mwana wa Neri. Mfalme Daudi aliwaambia watumishi wake, “Je, hamjui kuwa leo mtu mkuu na mashuhuri amefariki katika Israeli? Ijapokuwa mmenipaka mafuta ili niwe mfalme, lakini leo mimi ni mnyonge. Hawa wana wa Seruya ni wakatili kupita kiasi. Mwenyezi-Mungu na awaadhibu waovu hawa sawasawa na uovu wao.” Ishboshethi mwana wa Shauli, aliposikia kwamba Abneri ameuawa huko Hebroni, alivunjika moyo na watu wote wa Israeli walifadhaika. Ishboshethi mwana wa Shauli, alikuwa na watu wawili waliokuwa viongozi wa kikosi cha uvamizi; mmoja aliitwa Baana na mwingine Rekabu. Hao walikuwa wana wa Rimoni, mtu wa kabila la Benyamini kutoka mji wa Be-erothi, (kwa maana Be-erothi pia ulikuwa mali ya kabila la Benyamini). Wakazi wa Be-erothi walikimbilia Gitaimu, na wameishi huko kama wageni hadi leo. Yonathani mwana wa Shauli, alikuwa na mtoto aliyelemaa miguu yake yote miwili. Mtoto huyo aliitwa Mefiboshethi. Mefiboshethi alikuwa na umri wa miaka mitano habari za kifo cha Shauli na Yonathani ziliposikika kutoka Yezreeli. Yaya aliyekuwa anamtunza aliposikia kuwa Shauli na Yonathani wameuawa huko Yezreeli, alimchukua Mefiboshethi akakimbia naye. Lakini alipokuwa anakimbia kwa haraka mtoto huyo alianguka, naye akalemaa. Rekabu na Baana wana wa Rimoni Mbeerothi, wakaenda nyumbani kwa Ishboshethi. Walifika huko adhuhuri, Ishboshethi alipokuwa anapumzika nyumbani kwake. Waliingia nyumbani wakijifanya kana kwamba wanataka kuchukua ngano, wakamkuta Ishboshethi amelala kitandani mwake ndani ya chumba chake cha kulala, wakamchoma mkuki tumboni. Baada ya kumwua hivyo hao ndugu wawili walimkata kichwa wakatoroka wakiwa wamekichukua. Walipitia njia ya Araba, wakasafiri usiku kucha. *** Halafu walichukua kichwa cha Ishboshethi na kumpelekea Daudi huko Hebroni. Nao wakamwambia mfalme Daudi, “Hiki ni kichwa cha Ishboshethi mwana wa Shauli ambaye ni adui yako, aliyekuwa anataka kuyaangamiza maisha yako. Mwenyezi-Mungu leo amekulipizia kisasi dhidi ya Shauli na wazawa wake.” Lakini Daudi akamjibu Rekabu na Baana, nduguye, wana wa Rimoni, Mbeerothi,. “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba yeye ameyakomboa maisha yangu kutokana na kila adui. Yule mtu aliyekuja kuniambia kuwa Shauli amekufa, akidhani kuwa ananiletea habari njema, nilimkamata na kumwua huko. Hivyo ikawa ndiyo zawadi niliyompa kutokana na taarifa yake. Je, mtu mwovu anapomuua mtu mwadilifu akiwa kitandani, nyumbani kwake, je, si haki kwangu kumlipiza kwa sababu ya kumwaga damu kwa kumwulia mbali toka duniani?” Daudi akawaamuru vijana wake, nao wakawaua. Wakawakata mikono yao na miguu yao. Halafu wakawatundika mtini kando ya bwawa huko Hebroni. Lakini walikichukua kichwa cha Ishboshethi na kukizika katika kaburi la Abneri huko Hebroni. Kisha makabila yote ya Israeli yalimwendea Daudi huko Hebroni, na kumwambia, “Tazama, sisi ni mwili na damu yako. Hapo awali, Shauli alipokuwa mfalme wetu wewe ndiwe uliyewaongoza Waisraeli vitani, na Mwenyezi-Mungu alikuambia ‘Utakuwa mchungaji wa watu wangu Israeli na utakuwa mkuu juu ya Israeli.’” Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme Daudi huko Hebroni; naye akafanya agano nao mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli. Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, na alitawala kwa muda wa miaka arubaini. Huko Hebroni, alitawala watu wa Yuda kwa muda wa miaka saba na miezi sita, na huko Yerusalemu alitawala watu wa Israeli pamoja na Yuda kwa muda wa miaka thelathini na mitatu. Baadaye mfalme na watu wake walikwenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo. Lakini wao wakamwambia, “Hutaingia mjini humu, kwani vipofu na vilema watakufukuzia mbali.” Walimwambia hivyo kwani walifikiri kuwa Daudi asingeweza kuingia mjini humo. Hata hivyo, mfalme Daudi aliiteka ngome ya Siyoni, yaani mji wa Daudi. Siku hiyo, Daudi alisema, “Mtu yeyote atakayewapiga Wayebusi na apitie kwenye mfereji wa maji ili kuwashambulia vilema na vipofu ambao roho yangu inawachukia.” Ndio maana watu husema, “Vipofu na vilema hawataingia nyumbani.” Daudi alikaa kwenye ngome hiyo, nao mji akauita, “Mji wa Daudi.” Daudi aliujenga mji kuuzunguka, akianzia Milo kuelekea ndani. Naye Daudi akazidi kuwa maarufu zaidi kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye. Kisha, mfalme Hiramu wa Tiro alituma wajumbe kwa Daudi; alimpelekea pia mierezi, maseremala na waashi ambao walimjengea Daudi ikulu. Hivyo, Daudi akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu amemwimarisha awe mfalme wa Israeli, na kwamba ameukuza ufalme wake kwa ajili ya watu wake wa Israeli. Daudi alijitwalia masuria na wake zaidi wa huko mjini Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni. Hao, wakamzalia watoto zaidi wa kiume na wa kike. Yafuatayo ndiyo majina ya watoto wa kiume, wake zake waliomzalia huko Yerusalemu: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, Ibhari, Elishua, Nefegi, Yafia, Elishama, Eliada na Elifeleti. Wafilisti waliposikia kwamba Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wote walitoka kwenda kumtafuta, lakini yeye alipata habari, akaingia ndani ya ngome. Wafilisti walifika na kujitawanya kwenye Bonde la Refaimu. Basi, Daudi alimwuliza Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Daudi, “Nenda, maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” Basi, Daudi akafika Baal-perasimu, na kuwashinda Wafilisti; halafu akasema, “Mwenyezi-Mungu amepita katikati ya adui zangu kama mafuriko ya maji yaendayo kasi.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-perasimu. Wafilisti waliziacha sanamu zao za miungu mahali hapo, naye Daudi na watu wake wakazichukua. Kwa mara ya pili, Wafilisti walifika tena na kujitawanya kwenye bonde la Refaimu. Daudi alipomwomba Mwenyezi-Mungu shauri, Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiwashambulie kutoka hapa ulipo, bali zunguka na kuwashambulia kutoka mkabala wa miti na miforosadi. Na mara mtakaposikia vishindo vya gwaride kwenye vilele vya miforosadi hiyo, hapo jipe moyo kwani nitakuwa nimetoka ili kukutangulia kulipiga jeshi la Wafilisti.” Daudi alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, naye akawapiga Wafilisti kutoka Geba hadi Gezeri. Kwa mara nyingine, Daudi aliwakusanya wale askari bora wa Israeli, jumla yao 30,000. Daudi aliondoka akaenda pamoja na watu wake wote aliokuwa nao kutoka Baala-yuda, kwenda kulichukua toka huko sanduku la Mungu linaloitwa kwa jina lake Mwenyezi-Mungu wa Majeshi, akaaye kwenye kiti chake cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa. Basi, wakalichukua sanduku la Mungu kutoka katika nyumba ya Abinadabu iliyokuwa mlimani, wakalibeba juu ya gari jipya. Uza na Ahio wana wa Abinadabu wakawa wanaliendesha gari hilo jipya, likiwa na sanduku hilo la Mungu, naye Ahio akiwa anatangulia mbele ya sanduku hilo. Daudi na watu wote wa Israeli, wakawa wanaimba nyimbo na kucheza kwa nguvu zao zote, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Walipiga ala za muziki zilizotengenezwa kwa mvinje: Vinubi, vinanda, matari, kayamba na matoazi. Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Nakoni, Uza aliunyosha mkono wake na kulishika sanduku la Mungu kwa sababu wale ng'ombe walijikwaa. Hapo, hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Uza. Mungu akamuua palepale. Uza akafa papo hapo kando ya sanduku la Mungu. Naye Daudi alikasirika kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alimwadhibu Uza kwa hasira. Hivyo, mahali hapo pakaitwa Peres-uza mpaka hivi leo. Siku hiyo Daudi alimwogopa Mwenyezi-Mungu akasema, “Sasa litanijiaje sanduku la Mwenyezi-Mungu?” Kwa hiyo, Daudi hakuwa tayari kulipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu ndani ya mji wa Daudi, bali Daudi alilipeleka nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku hilo la Mwenyezi-Mungu lilikaa nyumbani kwa Obed-edomu kwa muda wa miezi mitatu; naye Mwenyezi-Mungu akambariki Obed-edomu pamoja na jamaa yake. Mfalme Daudi aliposikia kuwa Mwenyezi-Mungu ameibariki jamaa ya Obed-edomu na vitu vyote alivyokuwa navyo kwa sababu ya sanduku la Mungu, akaenda kulichukua sanduku la agano kutoka nyumbani kwa Obed-edomu na kulipeleka kwenye mji wa Daudi kwa shangwe. Watu wale waliolibeba sanduku la Mwenyezi-Mungu kila walipopiga hatua sita, Daudi alitoa tambiko: Fahali na ndama mmoja mnono. Daudi akiwa amejifunga kizibao cha kuhani kiunoni mwake alicheza kwa nguvu zake zote mbele ya Mwenyezi-Mungu. Hivyo, yeye na Waisraeli wote walilipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu hadi mjini mwa Daudi kwa shangwe na sauti kubwa ya tarumbeta. Sanduku la Mwenyezi-Mungu lilipokuwa linaingia katika mji wa Daudi, Mikali binti Shauli alichungulia dirishani akamwona mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele ya Mwenyezi-Mungu; basi, akamdharau moyoni mwake. Kisha waliliingiza sanduku la Mwenyezi-Mungu ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelipiga hapo na kuliweka mahali pake. Naye Daudi akatoa tambiko za kuteketezwa na tambiko za amani mbele ya Mwenyezi-Mungu. Daudi alipomaliza kutoa tambiko za kuteketezwa na za amani, aliwabariki watu kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi, na akawagawia watu wote, kundi lote la Waisraeli, wanaume na wanawake, kila mmoja, mkate, kipande cha nyama na mkate wa zabibu. Baadaye, watu wote waliondoka, kila mtu akarudi nyumbani kwake. Daudi aliporudi nyumbani kwake ili kuibariki jamaa yake, Mikali, binti Shauli, alikwenda kumlaki, akasema, “Ajabu ya mfalme wa Israeli kujiheshimu leo, kwa kujifunua uchi wake mbele ya watumishi wake wa kiume na wa kike kama mshenzi avuavyo mavazi yake mbele ya watu bila aibu!” Daudi akamwambia Mikali, “Nilikuwa mbele ya Mwenyezi-Mungu ambaye alinichagua mimi badala ya baba yako, na jamaa yake, ili kuniteua kuwa mkuu juu ya Israeli, watu wake Mwenyezi-Mungu, kwa hiyo mimi nitacheza tu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Nitajishusha mwenyewe zaidi kuliko sasa. Wewe utaniona kuwa si kitu, lakini hao watumishi wa kike uliowasema wataniheshimu.” Basi Mikali binti Shauli hakuwa na mtoto mpaka kufa kwake. Wakati mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika ikulu, naye Mwenyezi-Mungu amemuwezesha kuwa na amani na adui zake kila upande, mfalme Daudi akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama; mimi ninakaa katika nyumba iliyojengwa kwa mierezi, lakini sanduku la Mungu linakaa hemani.” Nathani akamwambia mfalme, “Nenda ufanye chochote unachofikiria moyoni mwako, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu yu pamoja nawe.” Lakini usiku uleule neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Nathani, “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Je, wewe utanijengea nyumba ya kukaa? Tangu siku ile nilipowatoa Waisraeli nchini Misri mpaka hivi leo sijaishi kwenye nyumba. Nimetembea kila mahali nikiwa ninakaa hemani. Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli wote nimemwuliza mtu yeyote wa Israeli ambaye nilimwamuru awachunge watu wa Israeli: Kwa nini hajanijengea nyumba ya mierezi? Kwa hiyo basi, mwambie mtumishi wangu Daudi: Mwenyezi-Mungu wa majeshi anasema hivi: Nilikutoa malishoni ulikokuwa unawachunga kondoo, ili uwe mkuu wa watu wangu Israeli. Tangu wakati huo nimekuwa pamoja nawe kokote ulikokwenda na nimewaangamiza adui zako wote mbele yako. Nitakufanya kuwa maarufu kama wakuu wengine duniani. Nami nitawachagulia watu wangu wa Israeli mahali pa kuishi, niwapandikize, ili waishi mahali pao wenyewe, wasisumbuliwe tena. Nao watu wakatili wanaotumia nguvu hawatawatesa tena kama hapo awali, tangu wakati nilipowateua waamuzi juu ya watu wangu Israeli, nami nitakulinda kutokana na adui zako wote. Zaidi ya yote, mimi Mwenyezi-Mungu nakutangazia kuwa nitakujengea nyumba. Siku zako zitakapotimia na utakapofariki na kujiunga na babu zako, nitamfanya mmoja wa watoto wako wewe mwenyewe awe mfalme, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu na kiti chake cha enzi cha ufalme wake nitakiimarisha milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Akifanya maovu, nitamrudi kama wanadamu wanavyowarudi wana wao kwa fimbo. Lakini sitamwondolea fadhili zangu kama vile nilivyoziondoa kwa Shauli, niliyemwondoa mbele yako. Ukoo wako na ufalme wako vitadumu imara daima. Kiti chako cha enzi kitakuwa imara milele.’” Nathani alimweleza Daudi kila kitu ambacho alioneshwa katika maono hayo na Mungu. Kisha mfalme Daudi akaingia ndani na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu; halafu akaomba, “Mimi ni nani ee Bwana Mungu, na jamaa yangu ni nini hata ukaniinua mpaka hapa nilipo leo! Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Bwana Mungu; zaidi ya hayo umeiahidi jamaa yangu mambo makubwa katika miaka mingi ijayo; na kwamba umenijalia kuona hayo, Ee Bwana Mungu. Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi, mtumishi wako? Kwani wewe unanijua mimi mtumishi wako, ee Bwana Mungu! Kutokana na ahadi yako na kulingana na moyo wako, umetenda makuu hayo yote ili unijulishe mimi mtumishi wako. Kutokana na yale tuliyosikia, wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu; hakuna aliye kama wewe, na hakuna Mungu mwingine ila wewe. Tena ni watu gani duniani ambao wanaweza kufananishwa na watu wako wa Israeli, ambao Mungu wake alikwenda kuwakomboa ili wawe watu wake? Wewe ee Mungu ulijifanyia jina na kujitendea mambo makubwa na ya ajabu kwa ajili ya nchi yako mbele ya watu wako ambao kwa ajili yako mwenyewe uliwaokoa kutoka Misri, ukayafukuza mataifa na miungu yake mbele yao? Hata umewaimarisha watu wako wa Israeli kwa ajili yako mwenyewe, ili wawe watu wako milele; nawe ee Mwenyezi-Mungu umekuwa Mungu wao. Basi, sasa, ee Mwenyezi-Mungu, ikamilishe ile ahadi uliyosema kuhusu mimi mtumishi wako na kuhusu jamaa yangu kama ulivyoahidi. Nalo jina lako litatukuzwa milele, nao watu watasema, ‘Mwenyezi-Mungu wa majeshi ni Mungu juu ya Israeli!’ Na jamaa yangu, mimi Daudi mtumishi wako, itaimarika mbele yako. Maana wewe, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, umenifunulia mimi mtumishi wako, ukisema ‘Nitakujengea nyumba;’ ndio maana nina ujasiri kutoa ombi hili mbele yako. Sasa, ee Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ni kweli na umeniahidi mimi mtumishi wako jambo hili jema; kwa hiyo, nakuomba nyumba yangu mimi mtumishi wako ipate kudumu milele mbele yako; kwani wewe umesema hivyo, pia kwa baraka zako nyumba yangu itabarikiwa milele.” Baada ya hayo, Daudi aliwapiga, akawashinda Wafilisti. Akauteka mji wa Metheg-ama kutoka utawala wa Wafilisti. Kisha aliwashinda Wamoabu. Aliwapanga katika mistari mateka hao, na kuwalaza chini. Aliamuru wale waliokuwa katika mistari miwili wauawe na wale wa mstari wa tatu waachwe hai. Hivyo, Wamoabu wakawa watumishi wake Daudi na wakawa wanamlipa kodi. Daudi pia alimshinda Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba. Daudi alipata ushindi huu wakati Hadadezeri alipokuwa njiani kwenda kulirudisha eneo la mto Eufrate kuwa chini ya utawala wake. Daudi aliteka wapandafarasi 1,700, na askari wa miguu 20,000. Kisha Daudi alikata mishipa ya miguu ya nyuma ya farasi wote wa magari, ila alibakiza farasi wa kutosheleza magari 100. Nao Waaramu wa Damasko walipokwenda kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi aliwashambulia na kuwaua watu 22,000. Halafu Daudi aliweka kambi za kijeshi katika mji wa Waaramu wa Damasko. Basi, Waaramu wakawa watumishi wake na wakawa wanamlipa kodi. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda. Daudi alizichukua ngao za dhahabu walizobeba wanajeshi wa Hadadezeri na kuzipeleka Yerusalemu. Pia alichukua shaba nyingi sana kutoka miji ya Beta na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri. Wakati Toi, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri, alimtuma mwanawe Yoramu kwa mfalme Daudi kumpelekea salamu na pongezi kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri na kumshinda. Maana Hadadezeri alipigana na Toi mara nyingi. Yoramu alimpelekea Daudi zawadi za vyombo vya fedha, dhahabu na shaba. Zawadi hizo, pamoja na fedha na dhahabu alizokuwa ameziteka kwa mataifa yote aliyoyashinda, aliziweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, yaani kutoka Edomu, Moabu, Amoni, Filistia, Amaleki, pamoja na nyara alizoteka kwa mfalme Hadadezeri, mwana wa Rehobu mfalme wa Soba. Daudi alijiongezea umaarufu wake. Alipokuwa anarudi baada ya kumshinda Hadadezeri, aliwaua Waedomu 18,000, katika Bonde la Chumvi. Akaweka kambi za kijeshi katika Edomu yote. Nao Waedomu wote wa huko wakawa watumishi wake. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda. Hivyo, Daudi akatawala juu ya Israeli yote, akahakikisha watu wake wote wanatendewa haki ipasavyo. Yoabu mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa majeshi. Yehoshafati mwana wa Ahiludi, alikuwa mweka kumbukumbu. Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari, walikuwa makuhani. Seraya alikuwa katibu. Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa kiongozi wa Wakerethi na Wapelethi, nao wana wa Daudi wakawa makuhani. Siku moja, Daudi aliuliza, “Je, kuna mtu yeyote aliyesalia katika jamaa ya Shauli? Kama yuko, ningependa kumtendea wema kwa ajili ya Yonathani.” Kulikuwa na mtumishi wa jamaa ya Shauli aliyeitwa Siba. Siba aliitwa kwenda kwa Daudi. Mfalme Daudi alimwuliza, “Je wewe ndiye Siba?” Naye akamjibu, “Naam, mimi mtumishi wako ndiye.” Mfalme akamwuliza, “Je, hakuna mtu yeyote aliyesalia katika jamaa ya Shauli? Kama yuko, ningependa kumtendea wema wa Mungu.” Siba akamjibu, “Yuko mwana wa Yonathani, lakini yeye amelemaa miguu.” Mfalme akamwuliza, “Yuko wapi?” Siba akamjibu, “Yuko nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-debari.” Basi, mfalme Daudi akatuma watu, naye akaletwa kutoka nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-debari. Basi, Mefiboshethi mwana wa Yonathani, na mjukuu wa Shauli akaenda kwa mfalme Daudi, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme Daudi, akasujudu. Daudi akamwita, “Mefiboshethi.” Naye akamjibu, “Naam! Mimi hapa mtumishi wako.” Daudi akamwambia, “Usiogope. Mimi nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Ile ardhi yote iliyokuwa ya babu yako Shauli nitakurudishia. Nawe, daima utakula mezani pangu.” Mefiboshethi akasujudu, na kusema, “Mimi ni sawa na mbwa mfu; kwa nini unishughulikie hivyo?” Kisha, mfalme Daudi akamwita Siba mtumishi wa Shauli, akamwambia, “Ile mali yote iliyokuwa ya Shauli na jamaa yake nimempa mjukuu wa bwana wako. Wewe, watoto wako na watumishi wako mtakuwa mnamlimia Mefiboshethi na mtamletea mavuno ili mjukuu wa bwana wako awe daima na chakula. Lakini yeye atakula mezani pangu.” Wakati huo, Siba alikuwa na watoto wa kiume kumi na watano na watumishi ishirini. Kisha, Siba akamwambia mfalme, “Mimi mtumishi wako, nitafanya yote kulingana na amri yako.” Basi, Mefiboshethi akawa anapata chakula chake mezani pa Daudi, kama mmojawapo wa watoto wa mfalme. Mefiboshethi alikuwa na mtoto mdogo wa kiume aliyeitwa Mika. Watu wote wa jamaa ya Siba wakawa watumishi wa Mefiboshethi. Hivyo, Mefiboshethi aliyekuwa amelemaa miguu yake yote akawa anaishi mjini Yerusalemu, na kupata chakula chake mezani pa mfalme daima. Baada ya hayo mfalme Nahashi wa Waamori akafa, na mwanawe aliyeitwa Hanuni akawa mfalme badala ya baba yake. Mfalme Daudi akasema, “Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahashi kama baba yake alivyonitendea.” Hivyo, Daudi alituma wajumbe kumpelekea salamu za rambirambi. Nao wajumbe wa Daudi walipofika katika nchi ya Waamori, wakuu wa Waamori walimwambia bwana wao, Hanuni, “Je, unadhani kwamba Daudi kwa kukutumia watu wa kukufariji anamheshimu baba yako? Je, Daudi hakuwatuma watu hawa kwako ili kuuchunguza na kuupeleleza mji halafu wauteke?” Basi, Hanuni aliwachukua wajumbe hao wa Daudi akamnyoa kila mmoja nusu ya ndevu zake, akayapasua mavazi yao katikati mpaka matakoni, kisha akawaacha waende zao. Waliona aibu mno kurudi nyumbani. Daudi alipopashwa habari alituma watu kuwalaki kwani hao wajumbe waliona aibu sana. Naye mfalme aliwaambia, “Kaeni mjini Yeriko, hata mtakapoota ndevu, kisha mrudi nyumbani.” Waamoni walipoona kuwa wamemchukiza Daudi, walikodi wanajeshi Waaramu 20,000 waendao kwa miguu, kutoka Beth-rehobu na Soba; wanajeshi 12,000, kutoka Tobu, na mfalme Maaka akiwa na wanajeshi 1,000. Naye Daudi aliposikia habari hizo, alimtuma Yoabu kwenda na jeshi lote la mashujaa. Waamoni walitoka na kujipanga tayari kwa vita kwenye lango la mji wa Raba, mji wao mkuu; nao Waaramu kutoka Soba na Rehobu na watu kutoka Tobu na Maaka walijipanga nyikani. Yoabu alipoona kuwa vita ni vikali dhidi yake, mbele na nyuma, aliwateua baadhi ya wanajeshi Waisraeli hodari zaidi akawapanga kukabiliana na Waaramu. Wale wanajeshi wengine waliobaki aliwaweka chini ya uongozi wa ndugu yake Abishai, naye akawapanga ili wakabiliane na Waamoni. Yoabu akamwambia Abishai, “Ikiwa Waaramu wananizidi nguvu, utanisaidia lakini kama Waamoni wanakuzidi nguvu, nitakuja kukusaidia. Lakini jipe moyo! Tupigane kiume kwa ajili ya watu wetu na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye Mwenyezi-Mungu atutendee lile analoona ni jema kwake.” Basi, Yoabu na watu wake walisonga mbele kwenda kupigana na Waaramu, nao Waaramu walikimbia. Waamoni walipoona kuwa Waaramu wamekimbia, nao pia walimkimbia Abishai na kuingia mjini. Yoabu akaacha kupigana na Waamoni, akarudi Yerusalemu. Lakini Waaramu walipoona kwamba wameshindwa na Waisraeli, walijikusanya pamoja. Hadadezeri aliagiza Waaramu waliokuwa ngambo ya mto Eufrate waletwe, wapelekwe huko Helamu wakiongozwa na Shobaki kamanda wa jeshi la Hadadezeri. Daudi alipopata habari, aliwakusanya pamoja Waisraeli wote, akavuka mto Yordani na kwenda mpaka Helamu. Nao Waaramu walijipanga tayari kwa vita dhidi ya Daudi, wakaanza kupigana naye. Lakini Waaramu walikimbia mbele ya Waisraeli. Daudi aliwaua Waaramu 700 waliokuwa madereva wa magari ya vita, wapandafarasi 40,000. Pia alimwumiza Shobaki kamanda wa jeshi lao, naye akafia papo hapo. Kisha wafalme wote waliokuwa watumishi wa Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Waisraeli, walifanya mapatano ya amani na Israeli, nao wakawa watumishi wa Israeli. Hivyo Waaramu hawakuthubutu kuwasaidia Waamoni tena. Hata ikawa katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati ambapo wafalme huenda vitani, Daudi alimtuma Yoabu na maofisa wake pamoja na Waisraeli wote kupigana; nao waliteka nyara Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi alibaki Yerusalemu. Siku moja, wakati wa jioni, Daudi aliamka kitandani akaenda kwenye paa ya ikulu. Alipokuwa anatembea huko juu, alimwona mwanamke mmoja akioga na mwanamke huyo alikuwa mzuri sana. Daudi akatuma mtu kuuliza mwanamke huyo ni nani. Mtu huyo akamwambia Daudi “Mwanamke huyo ni Bathsheba binti wa Eliabu, na ni mke wa Uria Mhiti.” Basi, Daudi alituma wajumbe wamlete. Basi Bathsheba akaja kwa Daudi, naye Daudi akalala naye; (mwanamke huyo alikuwa ndio tu amejitakasa baada ya hedhi yake); kisha akarudi nyumbani kwake. Mwanamke huyo akapata mimba, naye akatuma habari kwa Daudi kuwa ana mimba yake. Basi, Daudi akamtumia Yoabu ujumbe, “Mtume Uria, Mhiti kwangu.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi. Uria alipofika kwake, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, watu wote, na hali ya vita. Halafu Daudi alimwambia Uria, “Rudi nyumbani kwako ukanawe miguu yako.” Uria alitoka nyumbani kwa mfalme, na mara mfalme akampelekea zawadi. Lakini Uria hakurudi nyumbani kwake, bali alilala pamoja na watumishi wote wa bwana wake kwenye lango la ikulu. Daudi alipoambiwa kwamba Uria hakwenda nyumbani kwake, Daudi alimwuliza Uria, “Wewe umetoka safari, kwa nini hukuenda nyumbani kwako?” Uria alimjibu Daudi “Sanduku la agano, pamoja na majeshi yote ya Israeli na Yuda yanakaa kwenye vibanda vitani. Bwana wangu Yoabu na watumishi wake wote wamepiga kambi mbugani; je ni sawa mimi niende nyumbani nikale na kunywa na kulala na mke wangu? Kama uishivyo na roho yako inavyoishi, sitafanya kitu cha namna hiyo.” Kisha, Daudi akamwambia Uria, “Basi, kaa hapa leo pia, na kesho nitakuacha urudi.” Hivyo Uria akabaki mjini Yerusalemu siku hiyo. Siku iliyofuata, Daudi alimwalika Uria kula na kunywa huko kwake, akamfanya Uria alewe. Hata hivyo, usiku ule Uria hakwenda nyumbani kwake, ila alilala kwenye kochi lake pamoja na watumishi wa bwana wake. Asubuhi yake, Daudi alimwandikia Yoabu barua akampa Uria aipeleke kwa Yoabu. Katika barua hiyo Daudi aliandika hivi: “Mweke Uria kwenye mstari wa mbele, mahali ambako mapigano ni makali kabisa, kisha umwache huko na kurudi nyuma ili apigwe, afe.” Basi, Yoabu alipokuwa anauzingira mji alimweka Uria mahali ambapo alijua wazi wanajeshi wa adui walikuwa hodari sana. Wakazi wa mji huo walitoka katika mji wao na kupigana na Yoabu. Baadhi ya watumishi wa Daudi, waliuawa. Uria Mhiti naye aliuawa pia. Kisha, Yoabu alipeleka habari zote kwa Daudi akimweleza juu ya vita. Yoabu akamwamuru huyo mtumishi aliyemtuma hivi, “Baada ya kumweleza mfalme mambo yote kuhusu vita, akikasirika na kukuuliza, ‘Kwa nini mlikwenda karibu na mji mlipokuwa mnapigana? Hamkujua kwamba wangewapiga mishale kutoka kwenye kuta za mji wao? Nani alimuua Abimeleki mwana wa Yerubeshethi? Si alikuwa mwanamke mmoja mjini Thebesi ambaye alitupa jiwe la kusagia kutoka kwenye ukuta nalo likamuua Abimeleki? Kwa nini basi, mlikwenda karibu na ukuta?’ Basi, wewe utamwambia hivi, ‘Hata mtumishi wako Uria Mhiti, naye amekufa.’” Yule mjumbe alikwenda kwa Daudi na kumwambia yote aliyotumwa na Yoabu ayaseme. Yule mjumbe akamwambia Daudi, “Adui zetu walituzidi nguvu, wakatoka nje ya miji na kutushambulia nyikani. Hata hivyo sisi tuliwarudisha mpaka kwenye lango la mji. Halafu wakatupiga mishale sisi watumishi wako kutoka ukutani. Baadhi ya watumishi wako waliuawa. Hata mtumishi wako Uria, Mhiti, naye amekufa.” Daudi akamwambia yule mjumbe, “Utamwambia hivi Yoabu, ‘Jambo hili lisikusumbue kwani upanga hauna macho, vita huua yeyote yule. Bali, imarisha mashambulizi dhidi ya mji, hadi umeuangamiza mji huo’. Ndivyo utakavyomtia moyo Yoabu.” Bathsheba mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe Uria amekufa, alimwombolezea mumewe. Muda wa matanga ulipokwisha, Daudi aliagiza Bathsheba achukuliwe na kupelekwa nyumbani kwake. Bathsheba akawa mke wa Daudi, naye akamzalia Daudi mtoto wa kiume. Lakini jambo hilo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi-Mungu. Basi Mwenyezi-Mungu akamtuma nabii Nathani kwa Daudi. Nathani alimwendea Daudi, akamwambia, “Kulikuwa na wanaume wawili katika mji mmoja; mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo wengi na ng'ombe wengi. Lakini yule maskini alikuwa na mwanakondoo mdogo mmoja jike, ambaye alikuwa amemnunua. Alimtunza, naye akakua nyumbani mwake pamoja na watoto wake. Alimlisha mwanakondoo huyo chakula kilekile kama chake na kunywea kikombe chake naye pia alikuwa akimpakata kifuani. Mwanakondoo huyo alikuwa kama binti kwa yule mtu maskini. Siku moja, yule tajiri alifikiwa na mgeni. Basi, tajiri huyo hakutaka kuchukua mmoja wa kondoo wake mwenyewe au ng'ombe wake, amchinjie mgeni wake, ila alikwenda na kumnyanganya yule maskini mwanakondoo wake, akamchinjia mgeni wake.” Daudi aliposikia hayo, akawaka hasira dhidi ya yule tajiri. Akamwambia nabii Nathani, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai kwamba mtu aliyefanya jambo hilo anastahili kufa! Ni lazima amlipe yule maskini mwanakondoo huyo, tena mara nne, kwani ametenda jambo baya na hakuwa na huruma!” Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Mimi nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli na kukuokoa mikononi mwa Shauli. Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake zake wawe wako, tena nikakupa watu wa Israeli na wa Yuda uwatawale. Na kama haya yangekuwa kidogo mno kwako ningekuongezea mara mbili zaidi ya hayo. Kwa nini basi, umedharau neno langu mimi Mwenyezi-Mungu ukafanya uovu huu mbele yangu? Umemuua Uria Mhiti, kwa upanga, ukamchukua mke wake kuwa mkeo. Umewatumia Waamoni kumwua Uria vitani! Kwa hiyo basi, kwa kuwa umenidharau na umemchukua mke wa Uria Mhiti, kuwa mkeo, mauaji hayataondoka katika jamaa yako’. Sikiliza, Mwenyezi-Mungu asema, ‘Tazama, nitazusha maafa katika jamaa yako mwenyewe. Nitawachukua wake zako ukiona kwa macho yako mwenyewe na kumpa jirani yako, naye atalala nao hadharani. Wewe ulifanya jambo hilo kwa siri, lakini mimi nitayafanya haya mbele ya Waisraeli wote hadharani.’” Basi, Daudi akamwambia Nathani, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu.” Nathani akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amekusamehe dhambi yako, nawe hutakufa. Hata hivyo, kwa kuwa kwa tendo lako umemdharau kabisa Mwenyezi-Mungu, mtoto wako atakufa.” Kisha Nathani akarudi nyumbani kwake. Mwenyezi-Mungu alimpiga mtoto ambaye Bathsheba mkewe Uria alimzalia Daudi, naye akawa mgonjwa. Daudi alimwomba Mungu mtoto apate nafuu. Alikwenda chumbani kwake, na usiku kucha akalala sakafuni. Wazee waliokuwa wanamwangalia katika jumba hilo walimfuata na kumsihi aamke, lakini yeye alikataa, na hakula chakula chochote pamoja nao. Juma moja baadaye, mtoto huyo akafa. Watumishi wa Daudi waliogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwani walifikiri, “Mtoto huyo alipokuwa hai, tulizungumza naye, lakini hakutusikiliza. Sasa, tutamwambiaje kuwa mtoto wake amekufa? Huenda akajidhuru.” Daudi alipowaona watumishi wake wananongonezana, akagundua kuwa mtoto wake amekufa. Hivyo, akawauliza, “Je, mtoto amekufa?” Nao wakamjibu, “Naam! Amekufa.” Kisha, Daudi aliinuka kutoka sakafuni, akaoga, akajipaka mafuta na kubadilisha mavazi yake. Halafu akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu. Kisha akarudi nyumbani na alipotaka chakula, akapewa, naye akala. Ndipo watumishi wake wakamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilofanya? Mtoto alipokuwa hai, wewe ulifunga na kumlilia. Lakini alipokufa, umeinuka, ukala chakula.” Daudi akawajibu, “Ni kweli mtoto alipokuwa hai, nilifunga na kulia. Nilifanya hivyo kwani nilifikiri, ‘Nani anajua? Huenda Mwenyezi-Mungu akanirehemu ili mtoto aishi’. Lakini sasa amekufa, ya nini nifunge? Je, mimi naweza kumrudisha duniani? Siku moja, nitakwenda huko alikokwenda, lakini yeye hawezi kurudi kwangu.” Halafu Daudi akamfariji Bathsheba mkewe. Akalala naye, naye akapata mimba na kujifungua mtoto wa kiume, ambaye Daudi alimwita Solomoni. Mwenyezi-Mungu alimpenda mtoto huyo, naye akamtuma nabii Nathani kwa Daudi kuwa amwite mtoto huyo Yedidia kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu. Wakati huo, Yoabu aliushambulia Raba mji wa Waamoni, naye akauteka huo mji wa kifalme. Yoabu akatuma ujumbe kwa Daudi, “Nimeushambulia mji wa Raba, nami nimelikamata bwawa lao la maji. Sasa wakusanye watu wote waliosalia, upige kambi kuuzunguka na kuuteka. La sivyo, nikiuteka, utaitwa kwa jina langu.” Hivyo, Daudi akakusanya watu wote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka mji huo. Kisha akachukua taji ya mfalme wao kutoka kichwani pake. Uzito wa taji hiyo ya dhahabu ulikuwa kilo thelathini na tano; na ndani yake mlikuwamo jiwe la thamani. Naye Daudi akavikwa taji hiyo kichwani pake. Pia aliteka idadi kubwa sana ya nyara katika mji huo. Halafu aliwachukua watu wa mji huo, akawaweka wafanye kazi wakitumia misumeno, sururu za chuma, mashoka ya chuma na kuwatumia kufanya kazi katika tanuri ya matofali; hivyo ndivyo alivyoitenda miji yote ya Waamoni. Hatimaye Daudi na watu wote walirudi Yerusalemu. Absalomu, alikuwa na dada yake mzuri aliyeitwa Tamari. Muda si muda, Amnoni, mtoto mwingine wa kiume wa Daudi, akampenda sana Tamari. Amnoni aliteseka sana hata akajifanya mgonjwa kwa sababu ya dada yake Tamari hasa kwa vile Tamari alikuwa bikira, na ilionekana jambo lisilowezekana kwa Amnoni kufanya chochote naye. Lakini Amnoni alikuwa na rafiki aliyeitwa Yonadabu, mtoto wa Shama, ndugu ya Daudi. Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana. Yonadabu akamwambia Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme, kwa nini unakonda na unaonekana huna furaha kila siku? Mbona hutaki kuniambia.” Amnoni akamwambia, “Nampenda Tamari, dada ya ndugu yangu Absalomu.” Yonadabu akamwambia, “Wewe jilaze kitandani ukidai kuwa u mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona, wewe msihi ukisema, ‘Mruhusu dada yangu, Tamari, aje aniletee mkate nipate kula na aniandalie chakula mbele yangu ili nikione naye mwenyewe anilishe.’” Hivyo, Amnoni akaendelea kulala kitandani, akijifanya mgonjwa. Mfalme alipokwenda kumwona, Amnoni alimwambia, “Nakuomba, Tamari aje hapa anitengenezee mikate michache huku nikimwangalia. Halafu yeye mwenyewe anilishe.” Hivyo, Daudi alipeleka ujumbe kwa Tamari kwamba aende nyumbani kwa kaka yake Amnoni, akamtengenezee chakula. Tamari alikwenda huko, akamkuta Amnoni amelala. Akachukua unga, akaukanda, na kuoka mikate mbele ya Amnoni. Mikate hiyo ilipokuwa tayari, Tamari akaiopoa kutoka kikaangoni. Akampelekea Amnoni, lakini Amnoni alikataa kula, akasema kila mmoja na atolewe nje, na wote wakaondoka. Kisha, Amnoni akamwambia Tamari, “Sasa niletee mikate hiyo chumbani kwangu, halafu unilishe.” Tamari aliichukua mikate aliyoiandaa na kuipeleka chumbani kwa kaka yake Amnoni. Hapo, alipokuwa anampatia mikate hiyo, Amnoni alimkamata na kumwambia, “Njoo ulale nami.” Tamari akamwambia, “Sivyo, kaka yangu, usinilazimishe. Kitendo hiki hakifanyiki katika Israeli. Usifanye kitendo hiki cha kipumbavu. Kwa upande wangu, siwezi kuvumilia aibu hiyo. Na kwa upande wako, utakuwa mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, mimi nakusihi uzungumze na mfalme kwani hatakukataza kunioa.” Lakini Amnoni hakutaka kumsikiliza na kwa kuwa alimzidi nguvu, alimlazimisha, akalala naye. Kisha, Amnoni akamchukia Tamari kupita kiasi. Akamchukia Tamari kuliko alivyompenda hapo awali. Akamwambia Tamari, “Ondoka mara moja.” Tamari akamjibu, “Sivyo kaka yangu; ovu hili kubwa la kunifukuza ni baya zaidi kuliko lile ulilonitendea.” Lakini Amnoni hakutaka kumsikiliza. Akamwita kijana wake aliyemtumikia, akamwambia, “Mtoe mwanamke huyu mbele yangu. Na mlango uufunge kwa komeo.” Amnoni na yule kijana wakamtoa nje na kuufunga mlango kwa komeo. Tamari alikuwa amevaa vazi refu lenye mikono mirefu kwani hivyo ndivyo walivyovaa mabikira wa mfalme zamani hizo. Basi, Tamari alijipaka majivu kichwani, akalipasua vazi lake, akaweka mikono yake kichwani, halafu akaondoka huku analia kwa sauti. Kaka yake, Absalomu, alipomwona, alimwuliza, “Je, Amnoni kaka yako amelala nawe? Tulia dada yangu. Yeye ni kaka yako. Usilitie jambo hilo moyoni mwako.” Hivyo, Tamari aliishi katika nyumba ya Absalomu akiwa na huzuni na mpweke. Mfalme Daudi aliposikia jambo hilo alikasirika sana. Absalomu alimchukia Amnoni sana hata hakusema naye, kwa sababu alimshika kwa nguvu dada yake Tamari akalala naye. Baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na shughuli ya kuwakata kondoo wake manyoya mjini Baal-hasori, karibu na Efraimu. Akawaalika watoto wote wa kiume wa mfalme. Absalomu alimwendea mfalme Daudi, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako ninao wakata-kondoo manyoya. Nakuomba wewe mfalme pamoja na watumishi wako, mwende pamoja nami, mtumishi wako.” Mfalme akamjibu, “Sivyo, mwanangu, tusiende wote; tusije tukawa mzigo kwako.” Ingawa Absalomu alizidi kumsihi baba yake aende, lakini mfalme alikataa, ila alimpa baraka zake. Halafu, Absalomu akamwambia, “Kama huendi, basi, mruhusu ndugu yangu Amnoni twende naye.” Mfalme akamjibu, “Lakini kwa nini aende pamoja nanyi?” Lakini Absalomu alizidi kumsihi, na mwishowe mfalme akamruhusu Amnoni na wanawe wengine waende kwenye sherehe hiyo. Absalomu akawaambia watumishi wake, “Mwangalieni Amnoni atakapokuwa amekunywa divai na kufurahi. Nitakapowaambia, ‘Mpigeni Amnoni,’ muueni. Hiyo ni amri yangu kwenu. Jipeni moyo na muwe hodari.” Hivyo, watumishi wa Absalomu walimtendea Amnoni kama walivyoamriwa na Absalomu, kisha wana wa kiume wengine wa mfalme wakaondoka kila mmoja akapanda nyumbu wake na kukimbia. Walipokuwa bado njiani, Daudi alipata habari kuwa Absalomu amewaua watoto wake wote hakuna hata mmoja aliyesalia. Mfalme Daudi aliinuka, akararua mavazi yake kwa huzuni akalala chini. Hata na watumishi wake wote waliokuwa wamesimama karibu naye walirarua mavazi yao. Lakini Yonadabu, mwana wa Shimea, ndugu ya Daudi akamwambia, “Bwana wangu, usifikiri kuwa wanao wote wameuawa. Amnoni pekee ndiye aliyeuawa. Haya Absalomu aliyakusudia kuyafanya tangu wakati ule Amnoni alipomshika kwa nguvu dada yake Tamari na kulala naye. Hivyo, bwana wangu, usifikiri moyoni mwako kwamba watoto wako wote wamekufa. Ni Amnoni pekee ndiye aliyeuawa.” Lakini Absalomu alikuwa amekwisha kimbia. Naye kijana aliyekuwa na zamu ya ulinzi, mara akaona kundi kubwa la watu wanakuja kutokea mlimani katika barabara ya kutoka Horonaimu. Yonadabu akamwambia Daudi, “Tazama mfalme, wanao wanakuja kama nilivyokuambia mimi mtumishi wako.” Mara tu yule mtumishi alipomaliza kusema, wana wa kiume wa mfalme wakaingia, wakaanza kulia kwa sauti. Mfalme na watumishi wake wote, wakalia kwa uchungu. Lakini Absalomu alikimbilia kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa mji wa Geshuri. Mfalme Daudi akamwombolezea mwanawe Amnoni kwa siku nyingi. Absalomu alikimbilia mjini Geshuri, akakaa huko kwa muda wa miaka mitatu. Baada ya mfalme Daudi kutulia kutokana na kifo cha Amnoni, alianza kutamani kumwona mwanawe Absalomu. Yoabu mwana wa Seruya, alitambua kwamba maelekeo ya moyo wa Daudi yalikuwa kwa Absalomu tu. Hivyo alituma watu huko Tekoa ili wamtafutie mwanamke mwenye hekima. Walipomleta, akamwambia, “Jisingizie unafanya matanga. Vaa nguo za kuomboleza, usijipake mafuta, ila ujifanye kama mwanamke ambaye amekuwa katika maombolezo ya wafu kwa muda mrefu. Halafu nenda kwa mfalme ukamwambie yale ninayokuambia.” Kisha Yoabu akamwambia maneno ya kumwambia mfalme. Huyo mwanamke kutoka Tekoa akaenda kwa mfalme, akaanguka kifudifudi, mbele ya mfalme, akasujudu, akamwambia, “Ee mfalme, nisaidie.” Mfalme akamwambia, “Una shida gani?” Yule mwanamke akajibu, “Nasikitika, mimi ni mjane, mume wangu amekufa. Nilikuwa na watoto wa kiume wawili. Siku moja, walipokuwa mbugani, walianza kugombana. Kwa vile hapakuwa na mtu yeyote wa kuwaamua, mmoja akampiga mwenzake, akamuua. Sasa ndugu zangu wote wamenigeuka mimi mtumishi wako; wanataka nimtoe kwao mtoto aliyemuua mwenzake ili wamuue kwa kuyaangamiza maisha ya ndugu yake. Hivyo, watamuua huyu ambaye sasa ndiye mrithi. Wakifanya hivyo, watazima kabisa tumaini langu lililobakia, na mume wangu hataachiwa jina wala mzawa duniani.” Mfalme akamwambia yule mwanamke, “Rudi nyumbani nitaamuru jambo lako liangaliwe.” Yule mwanamke kutoka Tekoa akasema, “Bwana wangu mfalme, hatia yote na iwe juu yangu na juu ya jamaa ya baba yangu. Hivyo, wewe na ufalme wako msiwe na hatia.” Mfalme akamwambia, “Mtu yeyote akikutishia mlete kwangu na hatakuja kukugusa tena.” Yule mwanamke akamwambia, “Tafadhali, mfalme, niombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili yule ndugu yangu ambaye angelipiza kisasi cha mauaji ya mwanangu asifanye hatia nyingine kubwa ya kumwua yule mtoto wangu mwingine.” Mfalme Daudi akamwambia, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, hakuna hata unywele mmoja wa mwanao utakaoanguka chini.” Yule mwanamke akamwambia, “Nakuomba, mimi mtumishi wako, uniruhusu niseme neno moja kwako mfalme.” Mfalme akamwambia, “Sema”. Yule mwanamke akamwambia, “Kwa nini basi, umepanga uovu huu dhidi ya watu wa Mungu? Kulingana na uamuzi wako juu ya jambo hilo wewe mwenyewe umejihukumu kuwa na hatia kwa sababu humruhusu mwanao arudi nyumbani kutoka alikokimbilia. Sisi sote lazima tutakufa. Sisi ni kama maji yaliyomwagika chini ambayo hayazoleki. Hata Mungu hafanyi tofauti kwa mtu huyu na tofauti kwa mwingine; yeye hutafuta njia ili waliopigwa marufuku, wakakimbia, wapate kurudi. Mimi nimekuja kuzungumza nawe, bwana wangu mfalme, kwani wamenitisha. Basi, mimi mtumishi wako, niliwaza kuwa, ‘Afadhali nikazungumze na mfalme, huenda akanitimizia mahitaji yangu mimi mtumishi wake. Maana mfalme atanisikiliza na kuniokoa mikononi mwa mtu ambaye anataka kuniangamiza mimi pamoja na mwanangu kutoka urithi wa Mungu’. Nami mjakazi wako nilifikiri kuwa, ‘Neno lake bwana wangu mfalme litanipa amani moyoni, kwani wewe bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kupambanua mema na mabaya.’ Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, awe pamoja nawe.” Ndipo mfalme alipomjibu yule mwanamke, “Usinifiche jambo lolote nitakalokuuliza.” Yule mwanamke akasema, “Sema bwana wangu mfalme.” Mfalme akamwuliza, “Je, Yoabu anahusika katika jambo hili?” Yule mwanamke akasema, “Kama uishivyo, bwana wangu mfalme, mtu hawezi kukwepa kulia au kushoto kuhusu jambo ulilosema bwana wangu mfalme. Yoabu yule mtumishi wako ndiye aliyenituma. Ni yeye aliyeniambia maneno yote haya niliyokuambia mimi mtumishi wako. Yoabu alifanya hivyo ili kubadilisha mambo. Lakini, wewe bwana wangu, una hekima kama ya malaika wa Mungu hata unaweza kujua mambo yote yaliyoko duniani.” Kisha, mfalme akamwambia Yoabu, “Sasa sikiliza, natoa kibali changu ili umrudishe nyumbani yule kijana Absalomu.” Yoabu alianguka chini kifudifudi, akasujudu na kumtakia mfalme baraka, akasema, “Leo, mimi mtumishi wako, bwana wangu mfalme, ninajua kuwa nimepata kibali mbele yako, kwa kulikubali ombi langu.” Hivyo, Yoabu aliondoka, akaenda Geshuri kumleta Absalomu mjini Yerusalemu. Lakini mfalme akasema, “Absalomu aishi mbali nami; aishi nyumbani kwake. Asije hapa kuniona.” Hivyo, Absalomu akawa anaishi mbali, nyumbani kwake na hakumwona mfalme Daudi. Katika Israeli yote, hakuna yeyote aliyesifiwa kwa uzuri kama Absalomu. Tangu nyayo zake hadi utosini mwake, Absalomu hakuwa na kasoro yoyote. Kila alipokata nywele zake, (na kila mwishoni mwa mwaka alikata nywele zake kwani zilikuwa nzito), alipozipima, zilikuwa na uzito wa kilo mbili kulingana na vipimo vya kifalme. Absalomu alizaa watoto watatu wa kiume pamoja na binti mmoja jina lake Tamari. Tamari alikuwa mwanamke mzuri. Basi, Absalomu aliishi mjini Yerusalemu kwa muda wa miaka miwili mizima bila kumwona mfalme Daudi. Kisha, Absalomu alimtumia ujumbe Yoabu, ili aende kwa mfalme kwa niaba yake, lakini Yoabu akakataa. Absalomu akatuma ujumbe mara ya pili lakini Yoabu akakataa. Basi, Absalomu akawaambia watumishi wake, “Angalieni Yoabu ana shamba la shayiri karibu na langu. Nendeni mkalichome moto.” Kwa hiyo watumishi wa Absalomu wakalichoma moto shamba la Yoabu. Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu akamwuliza, “Kwa nini watumishi wako wamechoma moto shamba langu?” Absalomu akamjibu, “Tazama, nilikupelekea ujumbe, uje huku ili nikutume kwa mfalme, ukamwulize: ‘Kwa nini niliondoka Geshuri? Ingekuwa bora kwangu kubaki huko’. Sasa nisaidie nipate kumwona mfalme. Kama nina hatia basi, na aniue!” Kwa hiyo Yoabu akaenda na kumweleza mfalme maneno hayo yote, naye akamwita Absalomu, naye akaingia kwa mfalme, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme. Na mfalme akambusu Absalomu. Baada ya tukio hilo, Absalomu alijipatia gari, farasi na watu hamsini wa kumtangulia. Absalomu alizoea kuamka asubuhi na mapema na kwenda kusimama kwenye njia inayoelekea kwenye lango la mji. Mtu yeyote aliyekuwa na madai ambayo alitaka kuyapeleka kwa mfalme ili kupata uamuzi wake, Absalomu humwita mtu huyo kando na kumwuliza, “Unatoka mji gani?” Kama mtu huyo akisema ametoka mji fulani wa kabila la Israeli, Absalomu humwambia, “Madai yako ni ya haki kabisa. Lakini hakuna mtu yeyote aliyeteuliwa na mfalme kukusikiliza.” Tena, Absalomu humwambia, “Laiti mimi ningekuwa mwamuzi wa Israeli! Kila mtu mwenye madai au shauri angekuja kwangu, nami ningempa haki yake!” Zaidi ya hayo, Absalomu alinyosha mkono wake akamkumbatia na kumbusu mtu yeyote aliyekuja kumwinamia na kumsujudu. Basi, hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Waisraeli wote waliokuja kutafuta uamuzi wa mfalme. Kwa kufanya hivyo, Absalomu aliiteka mioyo ya Waisraeli. Baada ya miaka minne, Absalomu alimwambia mfalme, “Tafadhali uniruhusu niende huko Hebroni ili kutimiza nadhiri yangu ambayo nilimwekea Mwenyezi-Mungu; maana, mimi mtumishi wako, nilipoishi kule Geshuri katika Aramu, nilimwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri nikisema kuwa kama Mwenyezi-Mungu atanirudisha mjini Yerusalemu basi, nitamwabudu yeye.” Mfalme akamwambia, “Basi, nenda kwa amani.” Absalomu akaondoka kwenda Hebroni. Lakini Absalomu alituma wajumbe kwa siri katika makabila yote ya Israeli, wakasema, “Mara moja mtakaposikia mlio wa tarumbeta, semeni, ‘Absalomu ni mfalme katika Hebroni!’” Absalomu alipokwenda huko Hebroni, alikwenda na watu 200 aliowaalika kutoka Yerusalemu, nao walikwenda huko kwa nia njema, wala hawakujua chochote kuhusu mpango wa Absalomu. Wakati Absalomu alipokuwa akitoa tambiko, alituma ujumbe mjini Gilo kumwita Ahithofeli, Mgilo, aliyekuwa mshauri wa mfalme Daudi. Uasi wa Absalomu ukazidi kupata nguvu na watu walioandamana naye wakazidi kuongezeka. Mjumbe fulani alipomwendea Daudi na kumwambia, “Watu wa Israeli wamevutwa na Absalomu!” Basi, Daudi akawaambia watumishi wake waliokuwa naye mjini Yerusalemu, “Inukeni tukimbie, la sivyo, hatutaweza kumwepa Absalomu. Tufanye haraka kuondoka asije akatuletea maafa na kuuangamiza mji kwa mapanga.” Lakini watumishi wake wakamwambia, “Sisi watumishi wako, bwana wetu mfalme, tuko tayari kufanya lolote unaloamua.” Basi, mfalme akaondoka pamoja na jamaa yake, lakini akawaacha masuria wake kumi wakishughulika na kazi za nyumbani. Mfalme akaondoka pamoja na watu wake wote. Lakini akatua kidogo walipofikia nyumba ya mwisho mjini. Watumishi wote wa mfalme, Wakerethi wote, Wapelethi wote, pamoja na Wagiti 600 waliomfuata mfalme Daudi kutoka mji wa Gathi, waliondoka pamoja naye wakimtangulia. Kisha, mfalme Daudi alipomwona Itai, Mgiti, alimwambia, “Kwa nini hata wewe umeondoka pamoja nasi? Rudi ukakae na huyo mfalme kijana. Maana wewe ni mgeni huku, tena ni mkimbizi kutoka nyumbani kwenu. Wewe ulikuja huku juzijuzi tu. Je, nikufanye mtu wa kutangatanga pamoja nasi, nikijua kuwa sijui hata kule ninakoenda? Rudi nyumbani pamoja na ndugu zako. Naye Mwenyezi-Mungu akuoneshe fadhili zake na uaminifu.” Lakini Itai akamjibu mfalme, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na wewe bwana wangu mfalme uishivyo, popote utakapokuwa, ikiwa ni kwa kufa au ni kwa kuishi, nami mtumishi wako nitakuwapo.” Basi, Daudi akamwambia Itai, “Nenda basi, endelea mbele.” Hivyo, Itai, Mgiti, akapita yeye mwenyewe pamoja na watoto wake. Daudi alipokuwa akipita pamoja na watu wake, watu wote nchini kote walilia kwa sauti. Mfalme Daudi akavuka kijito cha Kidroni pamoja na watu wote, wakapita kuelekea jangwani. Kuhani Abiathari akatoka, hata na kuhani Sadoki akatoka pamoja na Walawi wote huku wamelibeba sanduku la agano la Mungu. Wakaliweka chini lile sanduku la Mungu, mpaka watu wote walipopita kutoka mjini Yerusalemu. Kisha mfalme akamwambia Sadoki, “Lirudishe sanduku la agano la Mungu mjini. Kama ninakubalika mbele ya Mwenyezi-Mungu, bila shaka atanirudisha na kunijalia kuliona tena sanduku lake na kuyaona maskani yake. Lakini ikiwa Mwenyezi-Mungu hapendezwi nami basi, mimi niko tayari; na anitendee lolote analoona jema kwake.” Mfalme Daudi akamwambia tena Sadoki, “Tazama, mchukue mwanao Ahimaasi na Yonathani mwana wa Abiathari mrudi nyumbani kwa amani. Lakini nitakuwa nikingojea penye vivuko huku nyikani, mpaka nitakapopata habari kutoka kwako.” Kwa hiyo Sadoki na Abiathari wakalirudisha sanduku la agano la Mungu mjini Yerusalemu, wakabaki humo. Lakini Daudi aliendelea, akapanda Mlima wa Mizeituni huku analia, bila viatu na kichwa chake kimefunikwa. Hata watu wote waliokuwa pamoja naye walivifunika vichwa vyao wakawa wanapanda mlima huku wanalia. Wakati huo, Daudi aliambiwa kuwa hata Ahithofeli alikuwa mmoja wa waasi waliojiunga na Absalomu. Lakini Daudi akaomba akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu nakuomba, uufanye mpango wa Ahithofeli usifanikiwe.” Daudi alipofika kwenye kilele cha mlima, mahali pa kumwabudia Mungu, mtu mmoja jina lake Hushai kutoka Arki alikuja ili kumlaki, mavazi yake yakiwa yameraruka na kichwani pake kuna mavumbi. Daudi akamwambia, “Ukienda pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu. Lakini kama utarudi mjini Yerusalemu na kumwambia Absalomu, ‘Nitakuwa mtumishi wako, ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako, hapo awali’; basi utanifanyia mpango wa Ahithofeli usifanikiwe. Makuhani Sadoki na Abiathari wako pamoja nawe mjini! Basi, chochote utakachosikia kutoka nyumbani kwa mfalme, waambie makuhani Sadoki na Abiathari. Tazama, watoto wao wawili wa kiume, Ahimaasi mwana wa Sadoki na Yonathani mwana wa Abiathari, wako pamoja nao. Na chochote mtakachosikia mtanipelekea habari kwa njia yao.” Basi, Hushai rafiki ya mfalme Daudi, akarudi mjini na wakati Absalomu alipokuwa anaingia mjini Yerusalemu. Daudi alipokuwa amekipita kidogo kilele cha mlima, Siba mtumishi wa Mefiboshethi alimlaki Daudi akiwa na punda wawili ambao walikuwa wametandikwa huku wamebeba mikate200, vishada 100 vya zabibu kavu, matunda 100 ya kiangazi na kiriba cha divai. Mfalme akamwuliza Siba, “Kwa nini umeleta vitu hivi?” Siba akamjibu, “Punda ni kwa ajili ya kupanda jamaa yako, mikate na matunda ya kiangazi ni kwa ajili ya vijana wote, nayo divai ni kwa ajili ya watakaozimia jangwani.” Mfalme akamwuliza, “Mwana wa bwana wako yuko wapi?” Siba akamwambia mfalme, “Yeye amebaki mjini Yerusalemu kwa sababu anadhani kwamba watu wa Israeli watamrudishia ufalme wa Shauli babu yake.” Mfalme akamwambia Siba, “Basi, yale yaliyokuwa mali ya Mefiboshethi sasa ni mali yako.” Siba akamwambia, “Nashukuru, bwana wangu mfalme, nami naomba nipate fadhili mbele yako daima.” Wakati Daudi alipowasili kule Bahurimu, alitokea mtu mmoja wa ukoo wa Shauli, jina lake Shimei mwana wa Gera, akaanza kumlaani Daudi kwa mfululizo. Akawa anamtupia mfalme Daudi mawe pamoja na watumishi wake. Watu wengine wote na mashujaa wakawa wanamzunguka Daudi upande wa kulia na kushoto. Shimei alimlaani Daudi akisema, “Nenda zako; nenda zako, wewe mtu mwuaji, mtu asiye na faida! Mwenyezi-Mungu amekulipiza kisasi kutokana na kumwaga damu yote ya jamaa ya Shauli, ambaye sasa wewe umechukua ufalme mahali pake. Sasa, Mwenyezi-Mungu amempa ufalme Absalomu mwanao. Tazama, sasa maangamizi yamekupata kwa sababu wewe ni mwuaji.” Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, “Kwa nini huyu mbwa mfu akulaani wewe bwana wangu mfalme? Niruhusu nimwendee, nami nitakikata kichwa chake.” Lakini mfalme akamwambia, “Je, kuna nini kati yangu na nyinyi wana wa Seruya? Ikiwa Mwenyezi-Mungu amemwambia ‘Mlaani Daudi’, nani sasa anaweza kuuliza ‘Kwa nini umefanya hivyo?’” Tena mfalme Daudi akamwambia Abishai na hata watumishi wake wote, “Ikiwa mtoto wangu mwenyewe anayawinda maisha yangu, je si zaidi mtu wa kabila la Benyamini? Nyinyi mwacheni anilaani kwani Mwenyezi-Mungu amemwagiza anilaani. Huenda Mwenyezi-Mungu akaangalia uovu wangu, naye akanilipa wema kwa laana hii ninayopata leo.” Hivyo mfalme Daudi na watu wake wakaendelea na safari huku Shimei akiwa anamfuata akimtupia mawe na kurusha juu vumbi dhidi ya mfalme Daudi. Shimei alikuwa akitembea kileleni mwa mlima, mkabala na mfalme Daudi. Kisha mfalme pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakafika mtoni wakiwa wamechoka. Basi wakapumzika. Wakati huo, Absalomu na watu wote wa Israeli wakaenda mjini Yerusalemu na Ahithofeli pamoja nao. Hushai kutoka Arki, rafiki ya Daudi, akamwendea Absalomu, akamwambia, “Uishi mfalme! Uishi mfalme!” Absalomu akamwuliza Hushai, “Je, huu ndio uaminifu wako kwa rafiki yako Daudi? Mbona hukuenda pamoja na rafiki yako?” Hushai akamjibu, “La! Maana yule ambaye amechaguliwa na Mwenyezi-Mungu, watu hawa na watu wote wa Israeli, huyo ndiye, mimi nitakuwa wake yeye, na nitabaki naye. Zaidi ya hayo, je, nitamtumikia nani? Je, si mwana wa rafiki yangu? Basi, kama nilivyomtumikia baba yako ndivyo nitakavyokutumikia wewe.” Ndipo Absalomu alipomwambia Ahithofeli, “Nishauri; tufanye nini?” Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Waingilie masuria wa baba yako ambao aliwaacha kuangalia nyumba yake. Baadaye watu wote wa Israeli watakaposikia kwamba umechukizwa na baba yako, hapo watu wote walio pamoja nawe watatiwa nguvu.” Hivyo, watu wakampigia Absalomu hema kwenye paa, naye akalala na masuria wa baba yake, watu wote wa Israeli wakiwa wanaona. Siku hizo, shauri lolote alilotoa Ahithofeli lilikuwa kama limetolewa na Mungu. Na shauri alilotoa Ahithofeli liliheshimiwa na Daudi na Absalomu. Zaidi ya Hayo, Ahithofeli alimwambia Absalomu, “Niruhusu nichague watu 12,000, niondoke na kumfuatia Daudi leo usiku. Nitamshambulia akiwa amechoka na amevunjika moyo, nami nitamtia wasiwasi. Watu wote walio pamoja naye watakimbia. Nitampiga mfalme peke yake, na kuwarudisha watu wengine wote kwako kama bibiarusi anavyokwenda nyumbani kwa mumewe. Wewe unayatafuta maisha ya mtu mmoja tu; na watu wengine watakuwa na amani.” Shauri hilo la Ahithofeli lilimpendeza Absalomu na wazee wote wa Israeli. Kisha, Absalomu akasema, “Mwiteni Hushai pia, yule mtu wa Arki, tusikie analotaka kusema.” Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu alimwuliza, “Hivyo ndivyo alivyosema Ahithofeli. Je, tufanye kama alivyotushauri? Kama sivyo, basi, tuambie lako.” Hushai akamwambia Absalomu, “Wakati huu, shauri alilolitoa Ahithofeli si jema.” Zaidi ya hayo, Hushai akamwambia, “Wewe unajua kwamba baba yako na watu wake ni mashujaa na kwamba wamekasirishwa kama dubu jike nyikani aliyenyanganywa watoto wake. Mbali na hayo, unajua kwamba baba yako ni bingwa wa vita. Yeye hatakaa usiku kucha pamoja na watu wake. Hata sasa amekwisha jificha kwenye mojawapo ya mapango yaliyoko huko au mahali pengine. Mtu yeyote atakayesikia kuuawa kwa watu katika mashambulizi ya kwanza atasema kuwa mauaji yametokea katika kundi la wafuasi wa Absalomu. Watu wako watakaposikia hivyo, hata wale watu wako walio shupavu, wenye mioyo shupavu kama ya simba, watavunjika moyo kabisa kwa hofu. Maana, Waisraeli wote wanajua kuwa baba yako ni shujaa na wote walio pamoja naye ni watu hodari. Shauri langu ni kwamba, uwakusanye kwako watu wote wa Israeli tangu Dani hadi Beer-sheba, upande wa kusini, wawe wengi kama mchanga wa bahari, na wewe mwenyewe binafsi uende vitani. Nasi tutamwendea Daudi mahali popote anapoweza kupatikana na tutamvamia kama umande unavyoiangukia ardhi. Basi, hakuna atakayesalia hata kama atakuwa yeye mwenyewe au watu wake wote walio pamoja naye. Iwapo atakimbilia mji fulani, basi, watu wote wa Israeli wataleta kamba na kuuburuta mji huo, hadi bondeni, kisibaki chochote hata jiwe dogo la mji huo.” Absalomu pamoja na watu wote wa Israeli wakasema, “Shauri la Hushai ni bora kuliko shauri la Ahithofeli.” Wakakataa shauri la Ahithofeli kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alikuwa amepanga kulishinda shauri jema la Ahithofeli ili aweze kumletea Absalomu maafa. Kisha Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari jinsi Ahithofeli na yeye mwenyewe walivyomshauri Absalomu na wazee wa Israeli. Akawaambia wampelekee Daudi habari upesi kwamba asilale usiku kwenye vivuko jangwani, bali, kwa njia yoyote ile, avuke na kuondoka ili asije akakamatwa na kuuawa, yeye pamoja na watu wake wote. Wakati huo, Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakimngojea karibu na Enrogeli, ili wasionekane na mtu yeyote wakiingia mjini. Kila mara mtumishi fulani wa kike alikuwa akiwapelekea habari nao wakaipeleka kwa mfalme Daudi. Lakini wakati huu, walionekana na kijana mmoja ambaye alikwenda na kumhabarisha Absalomu. Hivyo, Yonathani na Ahimaasi waliondoka haraka, wakaenda Bahurimu nyumbani kwa mtu fulani aliyekuwa na kisima uani kwake. Wakaingia humo kisimani na kujificha. Mwanamke mwenye nyumba hiyo akachukua kifuniko na kukifunika kisima hicho, halafu akaanika nafaka juu ya kifuniko. Habari hizo hazikujulikana. Watumishi wa Absalomu walipowasili kwa huyo mwanamke, wakamwambia, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?” Yule mwanamke akawaambia, “Wamekwenda ngambo ya kijito.” Walipowatafuta na kuwakosa, wakarudi mjini Yerusalemu. Baada ya watumishi wa Absalomu kuondoka, Yonathani na Ahimaasi walitoka kisimani, wakaenda kwa mfalme Daudi na kumpasha habari. Wakamwambia, “Ondoka, uende ngambo ya mto, kwa sababu Ahithofeli amemshauri Absalomu dhidi yako.” Kwa hiyo, Daudi akaondoka na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakavuka mto Yordani. Ilipofika asubuhi hakuna mtu aliyebaki nyuma bila kuvuka mto Yordani. Ahithofeli alipoona kwamba shauri lake halikufuatwa, alitandika punda wake, akaenda nyumbani, kwenye mji wake. Alipofika huko, alipanga vizuri mambo ya nyumbani kwake, akajinyonga. Akafariki na kuzikwa kwenye kaburi la baba yake. Basi, Daudi akaenda Mahanaimu. Absalomu akavuka mto Yordani na watu wote wa Israeli. Wakati huo, Absalomu alikuwa amemweka Amasa kuwa mkuu wa jeshi badala ya Yoabu. Amasa alikuwa mwana wa Yithra, Mwishmaeli. Mama yake aliitwa Abigali binti wa Nahashi, aliyekuwa dada yake, Seruya, mama yake Yoabu. Absalomu pamoja na watu wa Israeli walipiga kambi yao katika nchi ya Gileadi. Daudi alipowasili Mahanaimu, Shobi mwana wa Nahashi Mwamoni, kutoka mji wa Raba; Makiri mwana wa Amieli kutoka mji wa Lo-debari, pamoja na Barzilai Mgileadi kutoka mji wa Rogelimu, walipeleka vitanda, mabirika, vyombo vya udongo, ngano, shayiri, unga, bisi, kunde na dengu, asali, siagi, kondoo na jibini kutoka mifugo yao kwa ajili ya Daudi pamoja na watu aliokuwa nao. Maana walisema, “Watu hawa wana njaa, wamechoka na wana kiu kwa ajili ya kusafiri jangwani.” Daudi aliwahesabu watu waliokuwa pamoja naye, akawagawanya katika vikosi vya maelfu chini ya makamanda wao; na vikosi vya mamia, navyo chini ya makamanda wao. Daudi akalituma jeshi lake vitani katika vikosi vitatu: Theluthi moja chini ya Yoabu, theluthi ya pili chini ya Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu; na theluthi ya tatu chini ya Itai, Mgiti. Kisha mfalme Daudi akawaambia wote, “Mimi mwenyewe binafsi nitakwenda pamoja nanyi.” Lakini watu wakamwambia, “Hutatoka. Maana, ikiwa tutakimbia, hawatajali juu yetu. Ikiwa nusu yetu watakufa, pia hawatajishughulisha juu yetu. Lakini wewe una thamani kuliko watu 10,000 miongoni mwetu. Hivyo inafaa wewe ubaki mjini na kutupelekea msaada ukiwa mjini.” Mfalme akawaambia, “Lolote mnaloona ni bora kwenu, nitalitenda.” Hivyo, mfalme akasimama kando ya lango, huku jeshi lake likipita: Mamia na maelfu. Mfalme akawaamuru Yoabu, Abishai na Itai, “Kwa ajili yangu, mtendeeni yule kijana Absalomu kwa upole.” Watu wote walimsikia mfalme alipoamuru makamanda wake kuhusu Absalomu. Hivyo, jeshi la Daudi likaenda nyikani kupigana na watu wa Israeli. Mapigano hayo yalifanyika katika msitu wa Efraimu. Watumishi wa Daudi waliwashinda watu wa Israeli. Mauaji ya siku hiyo yalikuwa makubwa kwani watu 20,000 waliuawa. Mapigano hayo yalienea nchini kote na watu wengi walikufa msituni kuliko wale waliouawa kwa upanga vitani. Kisha Absalomu, akiwa amepanda nyumbu, alikutana na watumishi wa Daudi. Nyumbu huyo alipokuwa anapita chini ya tawi kubwa la mwaloni, hapo kichwa cha Absalomu kikakwama kwenye mwaloni. Absalomu akaachwa ananinginia juu. Lakini nyumbu wake akaendelea mbele. Mtu fulani aliyeona tukio hilo, akamwambia Yoabu, “Nimemwona Absalomu akininginia kwenye mwaloni.” Yoabu akamwambia mtu huyo, “Nini? Ulimwona Absalomu? Kwa nini, basi, hukumpiga papo hapo hadi ardhini? Ningefurahi kukulipa vipande kumi vya fedha na mkanda.” Lakini yule mtu akamwambia Yoabu, “Hata kama ningeuona uzito wa vipande 1,000 vya fedha mkononi mwangu, nisingeunyosha mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Maana, tulimsikia mfalme alipokuamuru wewe Abishai na Itai kwamba, kwa ajili yake, mumlinde kijana Absalomu. Kwa upande mwingine, kama ningemtendea kwa hila (na hakuna lolote linalofichika kwa mfalme) wewe mwenyewe ungeniruka.” Yoabu akamwambia, “Mimi sina wakati wa kupoteza pamoja nawe.” Hapo Yoabu akachukua mikuki midogo mitatu mkononi mwake, akaenda na kumchoma Absalomu moyoni, Absalomu akiwa bado hai kwenye tawi la mwaloni. Kisha, vijana kumi waliombebea silaha Yoabu, wakaja kumzunguka Absalomu, wakampiga na kumwua. Ndipo Yoabu akapiga tarumbeta na wanajeshi wote wakarudi kuwafuatia watu wa Israeli, kwani Yoabu aliwakataza. Wakamchukua Absalomu wakamtupa kwenye shimo kubwa msituni na kurundika rundo kubwa sana la mawe. Watu wote wa Israeli wakakimbia, kila mmoja nyumbani kwake. Absalomu, wakati wa uhai wake, alikuwa amejijengea na kujisimikia nguzo iliyoko kwenye Bonde la Mfalme, kwani alisema, “Mimi sina mtoto wa kiume wa kudumisha jina langu ili nikumbukwe.” Nguzo hiyo aliipa jina lake, na inaitwa “Nguzo ya Absalomu” mpaka leo. Kisha, Ahimaasi mwana wa Sadoki, akasema, “Niruhusu nikimbie kumpelekea mfalme habari hizi kuwa Mwenyezi-Mungu amemkomboa katika nguvu za adui zake.” Yoabu akamwambia, “Leo, hutapeleka habari hizo. Unaweza kupeleka habari hizo siku nyingine. Lakini leo hutapeleka habari zozote kwa kuwa mwana wa mfalme amekufa.” Ndipo Yoabu akamwambia mtu mmoja, Mkushi, “Wewe, nenda ukamweleze mfalme yale uliyoona.” Mkushi akainama kwa heshima mbele ya Yoabu, akaondoka mbio. Kisha Ahimaasi mwana wa Sadoki akamwambia Yoabu tena, “Haidhuru; niruhusu na mimi nimkimbilie yule Mkushi!” Yoabu akamwambia, “Mbona unataka kukimbia mwanangu? Wewe hutatuzwa lolote kwa habari hizi!” Ahimaasi akamwambia, “Haidhuru; nitakimbia.” Basi, Yoabu akamwambia, “Haya, kimbia.” Kisha Ahimaasi akakimbia akifuata njia ya nyikani akawahi kumpita yule Mkushi. Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili ya mji. Naye mlinzi wa lango akapanda ukutani hadi juu ya lango na alipoinua macho yake aliona mtu anakimbia peke yake. Huyo mlinzi akapaza sauti akamwambia mfalme. Mfalme akasema, “Kama yuko peke yake, lazima ana habari.” Yule mtu akazidi kukaribia. Mlinzi akamwona mtu mwingine anakimbia, akaita tena langoni akisema, “Tazama, mtu mwingine anakimbia peke yake!” Mfalme akasema, “Naye analeta habari.” Yule mlinzi akasema, “Naona kuwa yule anayekimbia zaidi ni Ahimaasi mwana wa Sadoki.” Mfalme akasema, “Huyo ni mtu mwema, anatuletea habari njema.” Ndipo Ahimaasi akamwambia mfalme kwa sauti kubwa, “Mambo yote ni sawa.” Akainama mbele ya mfalme, akasujudu na kusema, “Na atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ambaye amekukomboa kutoka watu walioinua mikono yao dhidi yako, bwana wangu mfalme.” Mfalme akamwambia, “Je, kijana Absalomu hajambo?” Ahimaasi akasema, “Wakati Yoabu aliponituma mimi mtumishi wako, niliona kulikuwa na kelele nyingi, lakini sikufahamu maana yake.” Mfalme akasema, “Kaa kando, na usimame hapo.” Basi, Ahimaasi akaenda kando na kusimama kimya. Ndipo na yule Mkushi akafika; naye akasema, “Kuna habari njema kwako bwana wangu mfalme! Maana Mwenyezi-Mungu leo hii amekukomboa kutoka nguvu za wale wote walioinuka dhidi yako.” Mfalme akamwuliza, “Je kijana Absalomu hajambo?” Mkushi akasema, “Maadui wako, bwana wangu mfalme, pamoja na wote wanaoinuka dhidi yako wakikutakia mabaya, wawe kama huyo kijana Absalomu.” Hapo mfalme alishikwa na huzuni kuu, akapanda kwenye chumba kilichokuwa juu ya lango na kulia. Alipokuwa anapanda, akawa analia akisema, “Mwanangu Absalomu, mwanangu Absalomu! Laiti ningalikufa badala yako! Ole, Absalomu mwanangu! Mwanangu!” Yoabu aliambiwa kwamba mfalme alikuwa akilia na kuomboleza juu ya kifo cha Absalomu. Kwa hiyo, ushindi wa siku hiyo uligeuzwa kuwa maombolezo kwa watu wote, waliposikia kuwa mfalme anamwombolezea Absalomu. Hivyo, siku hiyo, watu waliingia mjini kimyakimya kama watu wanaorudi mjini wakiona aibu kwa kukimbia vita. Mfalme alijifunika uso wake na kulia kwa sauti kubwa akisema, “Ole mwanangu Absalomu! Ole, Absalomu, mwanangu! Mwanangu!” Ndipo Yoabu alipoingia nyumbani kwa mfalme, akamwambia, “Leo umetuaibisha sisi watumishi wako wote ambao leo tumeyaokoa maisha yako, maisha ya watoto wako wa kiume, na maisha ya watoto wako wa kike, maisha ya wake zako na maisha ya masuria wako. Wewe unawapenda wale wanaokuchukia na unawachukia wale wanaokupenda. Umetuonesha waziwazi leo kwamba makamanda na watumishi wako hawana maana kwako. Naona kuwa leo, kama Absalomu angekuwa hai, na sisi sote tungalikuwa tumekufa, wewe ungefurahi. Sasa, simama uzungumze na watumishi wako kwa upole. Maana, naapa kwa Mwenyezi-Mungu kwamba, kama huendi kuzungumza nao, hakuna hata mmoja atakayebaki pamoja nawe leo jioni. Hili litakuwa jambo baya zaidi kwako kuliko maovu yote yaliyokupata tangu ujana wako hadi leo.” Kisha, mfalme akatoka akaenda, akaketi mahali pake karibu na lango. Watu wote walipoambiwa kuwa mfalme yuko langoni, wote walimwendea. Wakati huo, watu wote wa Israeli walikuwa wamekimbia, kila mmoja nyumbani kwake. Watu wote walikuwa wanashindana wao kwa wao katika makabila yote ya Israeli, wakisema, “Mfalme Daudi alitukomboa mikononi mwa adui zetu, alituokoa mikononi mwa Wafilisti. Lakini sasa ameikimbia nchi, akimkimbia Absalomu. Tena Absalomu ambaye tulimpaka mafuta awe mfalme wetu, sasa ameuawa vitani. Sasa, kwa nini hatuzungumzii juu ya kumrudisha mfalme Daudi?” Mfalme Daudi akatuma ujumbe kwa makuhani Sadoki na Abiathari, “Waambieni wazee wa Yuda: ‘Kwa nini wao wawe ndio wa mwisho kumrudisha mfalme nyumbani kwake? Ujumbe wa Israeli yote umenifikia mimi mfalme. Nyinyi ni ndugu zangu, nyinyi ni damu yangu; kwa nini muwe wa mwisho kunirudisha mimi mfalme nyumbani? Mwulizeni pia Amasa kama yeye si damu yangu. Tena Mungu aniue ikiwa simfanyi yeye kuwa kamanda wa jeshi langu tangu leo badala ya Yoabu.’” Hivyo, Daudi aliivuta mioyo ya watu wote wa Yuda kama mtu mmoja. Hivyo, wakampelekea ujumbe kusema “Rudi nyumbani, wewe na watumishi wako wote.” Basi, mfalme akaja mto Yordani na watu wote wa Yuda wakaja mpaka Gilgali kumlaki mfalme na kumvusha mtoni Yordani. Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini, kutoka Bahurimu, alifanya haraka kwenda pamoja na watu wengine ili kumlaki mfalme Daudi. Shimei alikwenda pamoja na Wabenyamini 1,000. Siba mtumishi wa jamaa ya Shauli, pamoja na watoto wake kumi na watumishi ishirini, walikwenda haraka mtoni Yordani kumtangulia mfalme Daudi. Basi, wakavuka kwenye kivuko ili kuisindikiza jamaa ya mfalme na kumfanyia mfalme yote aliyoyapenda. Shimei mwana wa Gera akaja, akajitupa mbele ya mfalme, akasujudu, wakati mfalme alipokuwa karibu kuvuka mto Yordani. Shimei akamwambia mfalme, “Nakuomba, bwana wangu mfalme, usinihesabu kuwa na hatia wala kukumbuka kosa nililofanya siku ile ulipokuwa ukiondoka mjini Yerusalemu. Nakuomba usiyaweke hayo maanani. Maana, mimi mtumishi wako ninajua kwamba nilitenda dhambi. Hii ndiyo sababu nimekuja leo, nikiwa wa kwanza katika kabila la Yosefu, kuja kukulaki wewe bwana wangu, mfalme.” Ndipo Abishai mwana wa Seruya akasema, “Je, si lazima Shimei auawe maana alimlaani mtu ambaye Mwenyezi-Mungu amemteua kwa kumpaka mafuta?” Lakini Daudi akasema, “Wana wa Seruya, sina lolote nanyi; kwa nini mjifanye kama maadui zangu leo? Je, auawe mtu yeyote katika Israeli siku ya leo? Je, sijui kuwa mimi ni mfalme wa Israeli siku ya leo?” Kisha, mfalme akamwambia Shimei, “Wewe hutauawa.” Mfalme akamwapia Shimei. Mefiboshethi mjukuu wa Shauli, alikwenda pia kumlaki mfalme Daudi. Tangu siku ile mfalme alipoondoka Yerusalemu mpaka aliporudi salama, Mefiboshethi alikuwa hajapata kuosha miguu yake, kukata ndevu zake na hakujali kufua nguo zake. Basi, ikawa alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, Daudi alimwuliza, “Je, Mefiboshethi, kwa nini hukuandamana pamoja nami?” Mefiboshethi akasema, “Ee bwana wangu mfalme, mtumishi wangu alinidanganya. Maana, mimi mtumishi wako, nilimwambia, ‘Nitandikie punda nipate kumpanda kwenda pamoja na mfalme,’ maana mimi mtumishi wako ni kilema. Sasa, amenisingizia kwako, ee bwana wangu mfalme. Lakini wewe, bwana wangu mfalme, uko kama malaika wa Mungu. Fanya lolote unaloona ni jema kwako. Maana, jamaa yote ya babu yangu walikuwa watu ambao wamestahili kuuawa mbele yako, bwana wangu mfalme. Lakini uliniweka mimi mtumishi wako miongoni mwa wale wanaokula mezani pako. Je, nina haki yoyote zaidi hata nikulilie mfalme?” Mfalme akamwambia, “Usiniambie zaidi juu ya mambo yako ya binafsi. Mimi nimekwisha amua kuwa wewe pamoja na Siba mtagawana nchi ya Shauli.” Lakini Mefiboshethi akamwambia mfalme, “Mruhusu Siba aichukue nchi yote peke yake. Mimi nimetosheka kwamba wewe bwana wangu mfalme umerudi nyumbani salama.” Barzilai Mgileadi alikuwa amefika kutoka Rogelimu. Alikuwa amekwenda pamoja na mfalme kwenye mto Yordani ili kumsindikiza hadi ngambo ya mto. Barzilai alikuwa mzee sana, mwenye umri wa miaka themanini. Naye Barzilai alikuwa amemtunza mfalme alipokaa huko Mahanaimu, kwa kuwa alikuwa tajiri sana. Basi, mfalme Daudi akamwambia Barzilai, “Twende wote huko Yerusalemu nami nitakutunza.” Lakini Barzilai akamwambia mfalme, “Je, nina miaka mingi ya kuishi ndipo niende nawe mfalme mpaka Yerusalemu? Mimi leo nina umri wa miaka themanini. Je, nina uwezo wa kubainisha yaliyo mazuri na yale yasiyo mazuri? Je, mimi mtumishi wako, naweza kutambua ladha ya kile ninachokula au kunywa? Je, nitaweza kutambua uzuri wa sauti za waimbaji wanaume au wanawake? Kwa nini mimi mtumishi wako niwe mzigo wa ziada kwako, bwana wangu mfalme? Mimi mtumishi wako nitakwenda nawe mwendo mfupi ngambo ya Yordani. Kwa nini, mfalme anilipe zawadi kubwa hivyo? Nakuomba, uniruhusu mimi mtumishi wako, nifie katika mji wangu, karibu na kaburi la baba yangu na mama yangu. Lakini huyu mtumishi wako Kimhamu, mruhusu aende pamoja nawe bwana wangu mfalme, na mtendee yeye lolote unaloona ni jema.” Mfalme akamwambia, “Kimhamu atakwenda nami, na nitamtendea lolote lililo jema kwako. Na lolote utakalotaka nikutendee, nitakutendea.” Ndipo watu wote wakavuka mtoni Yordani na mfalme naye akavuka. Mfalme akambusu na kumbariki Barzilai, na Barzilai akarudi nyumbani kwake. Mfalme aliendelea mpaka Gileadi, Kimhamu akawa anafuatana naye. Watu wote wa Yuda na nusu ya watu wa Israeli walikuwa wakimsindikiza mfalme. Kisha, watu wote wa Israeli wakaja kwa mfalme na kumwambia, “Kwa nini ndugu zetu watu wa Yuda walikuwa wamekuiba ukiwa njiani, wakakuvusha mto Yordani, wewe na jamaa yako, pamoja na watu wako?” Watu wa Yuda wakawaambia watu wa Israeli, “Kwa sababu mfalme ni ndugu yetu wa karibu. Kwa nini mnakasirika kuhusu jambo hili? Je, tumekula chochote wakati wowote kwa gharama ya mfalme? Au je, yeye ametupa zawadi yoyote?” Watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, “Tuna haki mara kumi juu ya mfalme, kuliko mlizo nazo nyinyi, na hata juu ya Daudi mwenyewe. Kwa nini, basi, mlitudharau? Je, sisi hatukuwa wa kwanza kusema kuwa mfalme wetu arudishwe?” Maneno ya watu wa Yuda yalikuwa makali kuliko maneno ya watu wa Israeli. Sasa ikawa kwamba huko Gilgali kulikuwa na mtu mmoja mlaghai aitwaye Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini. Basi Sheba alipiga tarumbeta, na kusema, “Hatuna fungu lolote kwa Daudi, hatuna sehemu yetu katika huyo mwana wa Yese. Enyi watu wa Israeli, kila mmoja na ajiendee hemani kwake!” Hivyo, watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi, wakamfuata Sheba mwana wa Bikri. Lakini watu wa Yuda walimfuata mfalme Daudi kwa uaminifu toka mto Yordani mpaka mjini Yerusalemu. Hatimaye, Daudi aliwasili nyumbani kwake mjini Yerusalemu. Mfalme aliwachukua masuria wake kumi ambao alikuwa amewaacha kuangalia nyumba yake, akawaweka kwenye nyumba moja chini ya ulinzi, akawatunza vizuri, lakini hakulala nao. Hivyo, masuria hao wakawa wametiwa ndani hadi siku za kufa kwao, wakaishi kana kwamba, walikuwa wajane. Kisha, mfalme akamwambia Amasa, “Nikusanyie watu wote wa Yuda katika siku tatu, na wewe mwenyewe uwepo.” Basi, Amasa akaenda kuwaita watu wa Yuda. Lakini akachelewa kurudi katika wakati ule aliopangiwa na mfalme. Daudi akamwambia Abishai, “Sasa, Sheba mwana wa Bikri, atatuletea madhara kuliko Absalomu. Chukua watumishi wangu, umfuatie Sheba asije akaingia kwenye miji yenye ngome akaponyoka, tusimwone tena.” Abishai akatoka akiwa pamoja na Yoabu, Wakerethi na Wapelethi pamoja na mashujaa wote. Hao wote waliondoka Yerusalemu kwenda kumfuatia Sheba mwana wa Bikri. Walipofika kwenye jiwe kubwa lililoko huko Gibeoni, Amasa akatoka kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa vazi la kijeshi, na ndani ya vazi hilo kulikuwa na mkanda ulioshikilia upanga kiunoni mwake ukiwa kwenye ala yake. Yoabu alipokuwa anakaribia, upanga wake ulichomoka alani ukaanguka chini. Yoabu akamwambia Amasa, “Je, hujambo ndugu yangu?” Yoabu akamshika Amasa kidevuni kwa mkono wa kulia kana kwamba anataka kumbusu. Lakini Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu. Basi, Yoabu akamchoma Amasa upanga tumboni, matumbo yake yakatoka nje, akafa. Yoabu hakumchoma upanga mara mbili. Kisha, Yoabu na nduguye Abishai wakaendelea kumfuatilia Sheba mwana wa Bikri. Mtu mmoja wa Yoabu akaja akasimama karibu na mwili wa Amasa, akasema, “Yeyote anayempenda Yoabu na yeyote anayempenda Daudi, na amfuate Yoabu!” Amasa alikuwa bado anagagaa kwenye damu yake katikati ya barabara kuu. Kwa hiyo, kila mtu aliyepita hapo, alipomwona, alisimama. Lakini yule mtu alipoona kwamba watu wote walikuja na kusimama hapo, aliuondoa mwili wa Amasa barabarani, akaupeleka shambani na kuufunika kwa nguo. Amasa alipoondolewa kwenye barabara kuu, watu wote sasa waliendelea kumfuata Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri. Sheba alipitia katika makabila yote ya Israeli mpaka mji wa Abeli wa Beth-maaka. Watu wote wa ukoo wa Bikri wakakusanyika na kumfuata. Watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakaenda kumzingira Sheba akiwa katika mji huo wa Abeli wa Beth-maaka. Walirundika kuuzingira mji, na ngome; halafu wakaanza kuubomoa ukuta ili kuuangusha chini. Kisha, mwanamke fulani mwenye hekima alisikika kutoka mjini akisema, “Sikieni! Sikieni! Mwambieni Yoabu aje nizungumze naye.” Yoabu akaenda karibu naye, huyo mwanamke akamwambia, “Je, wewe ni Yoabu?” Yoabu akasema, “Naam! Ni mimi.” Yule mwanamke akamwambia, “Nisikilize mimi mtumishi wako.” Yoabu akamwambia, “Nasikiliza.” Huyo mwanamke akamwambia, “Hapo kale watu walikuwa wakisema, ‘Waacheni watake shauri kutoka mji wa Abeli’. Ndivyo watu walivyoweza kutatua matatizo. Mimi ni mmojawapo wa wale wanaopenda amani na uaminifu katika Israeli. Sasa wewe unakusudia kuuharibu mji ambao ni kama mama katika Israeli. Kwa nini sasa unataka kuuangamiza mji ulio mali yake Mwenyezi-Mungu?” Yoabu akamjibu, “Kamwe maishani mwangu! Sina nia kuangamiza wala kuharibu. Ulivyosema si kweli! Lakini mtu mmoja kutoka sehemu ya milima ya Efraimu aitwaye Sheba mwana wa Bikri anataka kumwasi mfalme Daudi. Mtoeni huyo kwangu nami nitaondoka mjini kwenu.” Yule mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake kitarushwa kwako kupitia ukutani.” Kisha, huyo mwanamke akaenda kwa watu wote mjini kwa busara yake. Wakamkata kichwa Sheba mwana wa Bikri, wakakitupa nje kwa Yoabu. Kwa hiyo, Yoabu akapiga tarumbeta, na kuwatawanya watu wake kutoka mji huo wa Abeli; kila mtu akaenda nyumbani kwake. Kisha Yoabu akarudi kwa mfalme Daudi, mjini Yerusalemu. Sasa Yoabu alikuwa mkuu wa jeshi lote la Israeli. Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa mkuu wa Wakerethi na Wapelethi. Adoramu alikuwa msimamizi wa kazi za kulazimishwa; Yehoshafati alikuwa mwandishi wa kumbukumbu. Shausha alikuwa katibu; Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani. Ira, Myairi alikuwa pia kuhani wa Daudi. Wakati mmoja kulitokea njaa kali nchini Daudi akiwa mfalme. Njaa hiyo ilidumu miaka mitatu mfululizo. Daudi alimwomba Mwenyezi-Mungu shauri. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Shauli na jamaa yake wana hatia ya kumwaga damu kwa sababu aliwaua Wagibeoni.” Hivyo, mfalme Daudi akawaita Wagibeoni (Wagibeoni hawakuwa Waisraeli ila walikuwa mabaki ya Waamori. Ingawa watu wa Israeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Shauli alijaribu kuwaua wote kwani alikuwa na bidii ya upendeleo kwa watu wa Israeli na wa Yuda). Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitalipaje kwa maovu mliyotendewa ili mpate kuibariki nchi hii na watu wake Mwenyezi-Mungu?” Wagibeoni wakamwambia, “Kisa chetu na Shauli pamoja na jamaa yake si jambo la fedha au dhahabu. Wala si juu yetu kumwua yeyote katika nchi ya Israeli.” Mfalme akawauliza tena, “Sasa mnasema niwatendee nini?” Wao wakamwambia mfalme, “Shauli alikusudia kutuua sisi na kutuangamiza, asiache mtu wetu yeyote katika eneo lote la Israeli. Basi, tukabidhi watu saba kati ya wanawe wa kiume, nasi tuwanyonge mbele ya Mwenyezi-Mungu mlimani Gibea, kwa Shauli aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu.” Mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.” Lakini mfalme alimnusuru Mefiboshethi mwana wa Yonathani kwa sababu ya kiapo ambacho Daudi na Yonathani mwana wa Shauli walikuwa wamekula kati yao kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Lakini mfalme aliwachukua wana wawili ambao Rispa binti Ahiya alimzalia Shauli, Armoni na Mefiboshethi, pamoja na watoto wote watano wa kiume wa Mikali, binti Shauli ambao alimzalia Adrieli mwana wa Barzilai Mmeholathi. Watoto hao saba wa kiume Daudi aliwakabidhi kwa Wagibeoni, nao wakawatundika mlimani mbele ya Mwenyezi-Mungu, wote saba wakafa pamoja. Watoto hao waliuawa mwanzoni mwa mavuno ya shayiri. Kisha, Rispa binti Aya alichukua nguo ya gunia, akajitandikia mwambani. Alikaa hapo tangu mwanzo wa mavuno mpaka wakati wa mvua ulipowadia na kuinyeshea maiti. Wakati huo wote, aliwafukuza ndege wa angani na wanyama wa porini, usiku na mchana, ili wasifikie maiti hizo. Daudi aliposikia yale aliyofanya Rispa binti Aya, suria wa Shauli, alikwenda na kuichukua mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe kutoka wakazi wa Yabesh-gileadi, waliokuwa wameiiba kutoka mtaani huko Beth-sheani, ambako Wafilisti walikuwa wamemtundika Shauli na Yonathani siku ile Wafilisti walipomuua Shauli mlimani Gilboa. Basi, Daudi akairudisha mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe kutoka huko; halafu wakakusanya mifupa ya vijana saba waliotundikwa. Basi, watu wa Daudi wakaizika mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Sela katika kaburi la Kishi baba yake Shauli. Walifanya kila kitu ambacho mfalme aliamuru. Baada ya hayo, Mungu akayasikiliza maombi kuhusu nchi yao. Kisha Wafilisti walifanya vita tena na Waisraeli. Naye Daudi na watu wake wakaenda kupigana na Wafilisti. Daudi alichoka sana siku hiyo. Ishbi-benobu, mmojawapo wa wazawa wa majitu ambaye mkuki wake wa shaba ulikuwa na uzito wa karibu kilo tatu na nusu na aliyekuwa amejifunga upanga mpya alisema atamuua Daudi. Lakini Abishai mwana wa Seruya, alikwenda kumsaidia Daudi. Abishai alimshambulia yule Mfilisti na kumwua. Hivyo, watu wakamwapia Daudi wakisema, “Hutakwenda tena nasi vitani, la sivyo utaizima taa ya ufalme katika Israeli.” Baada ya hayo, kulitokea tena mapigano na Wafilisti huko Gobu. Huko Sibekai, Mhushathi, alimuua Safu aliyekuwa mmojawapo wa wazawa wa Warefai. Kulitokea tena mapigano na Wafilisti huko Gobu. Naye Elhanani mwana wa Yaareo-regimu, Mbethlehemu, alimuua Goliathi Mgiti, ambaye mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumanguo. Baadaye kulitokea tena vita huko Gathi ambako kulikuwa na mtu mmoja alikuwa mkubwa kwa kimo, na mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake vidole ishirini na vinne. Yeye pia alikuwa mzawa wa majitu. Alipowadhihaki Waisraeli, Yonathani mwana wa Shimei, nduguye Daudi, alimuua. Hao wanne walikuwa wazawa wa majitu huko Gathi, nao waliuawa na Daudi pamoja na watumishi wake. Daudi alimwimbia Mwenyezi-Mungu maneno ya wimbo ufuatao siku ile Mwenyezi-Mungu alipomkomboa mikononi mwa adui zake, na mkononi mwa Shauli. Alisema, “Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu, na mkombozi wangu. Mungu wangu, mwamba wangu, ninayemkimbilia usalama; ngao yangu, nguvu ya wokovu wangu, ngome yangu na kimbilio langu. Mwokozi wangu; unaniokoa kutoka kwa watu wakatili. Namwita Mwenyezi-Mungu astahiliye sifa anisaidie, nami naokolewa kutoka kwa adui zangu. “Maana mawimbi ya kifo yalinizingira, mafuriko ya maangamizi yalinivamia; kamba za kuzimu zilinizinga, mitego ya kifo ilinikabili. “Katika taabu yangu, nilimwita Mwenyezi-Mungu; nilimwita Mungu wangu. Toka hekaluni mwake aliisikia sauti yangu, kilio changu kilimfikia masikioni mwake. “Hapo, dunia ikatetemeka na kutikisika, misingi ya mbinguni ikayumbayumba na kuruka, kwani Mungu alikuwa amekasirika. Moshi ulifuka kutoka puani mwake, moto uunguzao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yalilipuka kutoka kwake. Aliinamisha anga, akashuka chini; na wingu jeusi chini ya miguu yake. Alipanda kiumbe chenye mabawa na kuruka, alionekana juu ya mabawa ya upepo. Alijizungushia giza pande zote, kifuniko chake kilikuwa mawingu mazito na mkusanyiko wa maji. Umeme ulimulika mbele yake, kulilipuka makaa ya moto. Mwenyezi-Mungu alinguruma kutoka mbinguni, Mungu Mkuu akatoa sauti yake. Aliwalenga adui mishale, akawatawanya, alirusha umeme, akawatimua. Mwenyezi-Mungu alipowakemea, kutokana na pumzi ya puani mwake, vilindi vya bahari vilifunuliwa, misingi ya dunia ikaonekana. “Mungu alinyosha mkono wake toka juu, akanichukua, kutoka kwenye maji mengi alininyanyua. Aliniokoa kutoka kwa adui yangu mwenye nguvu, aliniokoa kutoka kwa hao walionichukia maana walikuwa na nguvu nyingi kunishinda. Walinivamia nilipokuwa taabuni, lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa kinga yangu. Alinileta, akaniweka mahali pa usalama, alinisalimisha, kwani alipendezwa nami. “Mwenyezi-Mungu alinipa tuzo kadiri ya uadilifu wangu; alinituza kwa vile mikono yangu haina hatia. Maana, nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu, wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu. Nimeshika maagizo yake yote, sikuacha kufuata masharti yake. Mbele yake sikuwa na hatia, nimejikinga nisiwe na hatia. Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu, yeye anajua usafi wangu. “Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu, mwema kwa wale walio wema. Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu, lakini mkatili kwa watu walio waovu. Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu, lakini wawaangalia wenye majivuno kuwaporomosha. Ee Mwenyezi-Mungu, wewe u taa yangu, Mungu wangu, unayefukuza giza langu. Kwa msaada wako, wakishambulia kikosi; wewe wanipa nguvu ya kuruka kuta zake. Anachofanya Mungu hakina dosari! Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika; yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia. “Nani aliye Mungu isipokuwa Mwenyezi-Mungu? Nani aliye mwamba wa usalama ila Mungu wetu? Mungu huyu ndiye kimbilio langu imara, na ameifanya njia yangu iwe salama. Ameiimarisha miguu yangu kama ya paa, na kuniweka salama juu ya vilele. Hunifunza kupigana vita, mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba. Umenipa ngao yako ya kuniokoa; msaada wako umenifanya mkuu. Umenirahisishia njia yangu; wala miguu yangu haikuteleza. Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza, sikurudi nyuma mpaka wameangamizwa. Niliwaangamiza, nikawaangusha chini wasiweze kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita; uliwaporomosha adui chini yangu. Uliwafanya adui zangu wakimbie, na wale walionichukia niliwaangamiza. Walitafuta msaada, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa, walimlilia Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwajibu. Niliwatwanga na kuwaponda kama mavumbi ya nchi, nikawaponda na kuwakanyaga kama matope barabarani. “Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu wangu, umenifanya mtawala wa mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Wageni walinijia wakinyenyekea, mara waliposikia habari zangu walinitii. Wageni walikufa moyo; wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka. “Mwenyezi-Mungu yu hai! Asifiwe mwamba wangu! Atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu. Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi na kuyatiisha mataifa chini yangu. Ameniokoa kutoka adui zangu. Ee Mwenyezi-Mungu, ulinikuza juu ya wapinzani wangu na kunisalimisha mbali na watu wakatili. “Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa, ee Mwenyezi-Mungu, nitaliimbia sifa jina lako. Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa; humwonesha fadhili zake huyo aliyemweka wakfu, naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.” Yafuatayo ni maneno ya mwisho ya Daudi. Ni ujumbe wa Daudi mwana wa Yese; ujumbe wa mtu ambaye Mungu alimfanya awe mkuu. Mungu wa Yakobo alimteua Daudi kuwa mfalme na maneno yake Waisraeli walifurahi kuyaimba. “Roho ya Mwenyezi-Mungu imesema kwa njia yangu, aliyaweka maneno yake kinywani mwangu. Mungu wa Israeli amesema, Mwamba wa Israeli ameniambia, ‘Mtu anapowatawala watu kwa haki, atawalaye kwa kumcha Mungu, yeye ni kama mwanga wa asubuhi, jua linapochomoza asubuhi isiyo na mawingu; naam, kama mvua inayootesha majani ardhini’. Hivyo ndivyo Mungu alivyoujalia ukoo wangu. Maana amefanya nami agano la kudumu milele; agano kamili na thabiti. Naye atanifanikisha katika matakwa yangu yote. Lakini wasiomcha Mungu wote ni kama miiba inayotupwa tu, maana haiwezi kuchukuliwa kwa mkono; kuishika, lazima kutumia chuma au mpini wa mkuki. Watu hao wataangamizwa kabisa kwa moto.” Yafuatayo ni majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi: Yosheb-bashebethi, Mtakmoni, aliyekuwa kiongozi wa wale watatu, yeye alipigana kwa mkuki wake, akaua watu 800 wakati mmoja. Halafu aliyefuata miongoni mwa wale mashujaa watatu alikuwa Eleazari mwana wa Dodo, wa ukoo wa Mwahohi. Siku moja, Eleazari alikuwa pamoja na Daudi walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika kupigana vita. Waisraeli waliwakimbia Wafilisti. Lakini Eleazari alisimama imara na kupigana na Wafilisti mpaka mkono wake uliposhindwa kupinda, ukabaki umeshikilia upanga wake. Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu alijipatia ushindi mkubwa. Baada ya ushindi huo, Waisraeli walirudi mahali alipokuwa Eleazari na kujipatia nyara za bure kutoka kwa Wafilisti waliouawa. Shujaa wa tatu alikuwa Shama mwana wa Agee, Mharari. Wafilisti walikusanyika huko Lehi, mahali palipokuwa na shamba la dengu nyingi, nao Waisraeli waliwakimbia Wafilisti. Lakini alisimama imara katikati ya shamba hilo ili kulitetea, naye akawaua Wafilisti. Mwenyezi-Mungu alijipatia ushindi mkubwa. Kisha, mashujaa watatu kati ya wakuu thelathini waliteremka wakati wa mavuno wakamfikia Daudi kwenye pango huko Adulamu. Wakati huo jeshi la Wafilisti lilikuwa limepiga kambi katika bonde la Refaimu. Naye Daudi wakati huo alikuwa katika ngome, nalo jeshi la Wafilisti lilikuwa mjini Bethlehemu. Daudi akasema kwa hamu kubwa, “Laiti mtu angeweza kunipa maji ya kunywa kutoka katika kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango la mji!” Wale mashujaa wake watatu walitoka, wakapenya katikati ya kambi ya jeshi la Wafilisti, wakaenda na kuchota maji katika kisima cha Bethlehemu, karibu na lango la mji, wakamletea Daudi. Lakini Daudi alikataa kuyanywa, na badala yake, akayamwaga chini kama tambiko kwa Mwenyezi-Mungu, akisema, “Kamwe, sina haki ya kunywa maji haya, ee Mwenyezi-Mungu; je, haya si kama damu ya wale walioyahatarisha maisha yao kuyaleta maji haya?” Kwa hiyo, Daudi hakuyanywa maji hayo. Hayo ndiyo mambo waliyotenda wale mashujaa watatu. Abishai nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa mashujaa thelathini. Yeye alipigana kwa mkuki wake dhidi ya watu 300, akawaua, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. Je, huyo hakuwa mashuhuri zaidi miongoni mwa mashujaa watatu? Kwa hiyo akawa kamanda wao, lakini hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu. Naye Benaya mwana wa Yehoyada, kutoka Kabzeeli, alikuwa askari shujaa ambaye alifanya mambo mengi ya ajabu. Aliwaua mashujaa wawili kutoka Moabu, na siku moja wakati wa theluji, alishuka shimoni na kuua simba. Vilevile, aliliua jitu la Misri. Mmisri huyo alikuwa na mkuki, lakini Benaya alimwendea akiwa na fimbo tu, akamnyanganya mkuki huo, na kumwua Mmisri huyo kwa mkuki wake mwenyewe. Benaya, mwana wa Yehoyada alifanya mambo haya, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. Basi, akawa mashuhuri kati ya wale mashujaa thelathini, ingawa hakuwa kama wale mashujaa watatu. Na Daudi akampa cheo cha mkuu wa walinzi wake binafsi. Asaheli, nduguye Yoabu, alikuwa mmoja wa mashujaa thelathini. Mashujaa wengine wa Daudi walikuwa: Elhanani, mwana wa Dodo wa Bethlehemu; Shama, Mharodi; Elika, Mharodi; Helesi, Mpalti; Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoa; Abiezeri, Mwanathothi; Mebunai, Mhushathi; Salmoni, Mwahohi; Maharai, Mnetofathi; Helebu mwana wa Baana, Mnetofathi; Itai mwana wa Ribai, toka Gibea katika Benyamini; Benaya, Mpirathoni; Hidai, wa vijito vya Gaashi; Abialboni, Mwarbathi; Azmawethi, Mbahurimu; Eliaba, Mshaalboni; wana wa Yasheni; Yonathani; Shama, Mharari; Ahimu mwana wa Sharari, Mharari; Elifeleti mwana wa Ahasbai, Mmaaka; Eliamu mwana wa Ahithofeli, Mgiloni; Hesrawi, Mkarmeli; Paarai, Mwarbi; Igali mwana wa Nathani, Msoba; Bani, Mgadi; Seleki, Mwamoni; Naharai, Mbeerothi aliyekuwa mbeba silaha wa Yoabu mwana wa Seruya; Ira na Garebu, Waithri; na Uria, Mhiti. Wote pamoja walikuwa mashujaa thelathini na saba. Kwa mara nyingine, Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia Waisraeli, akamchochea Daudi dhidi yao, akamwambia awahesabu watu wa Israeli na watu wa Yuda. Hivyo, mfalme akamwambia Yoabu, na makamanda wa jeshi waliokuwa pamoja naye, “Nendeni katika makabila yote ya Israeli kutoka Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu ili nipate kujua idadi yao.” Lakini Yoabu akamwambia mfalme, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na awaongeze Waisraeli mara mia kuliko walivyo sasa, nawe bwana wangu mfalme upate kuona ongezeko hilo kwa macho yako mwenyewe. Lakini, kwa nini wewe bwana wangu mfalme unapendezwa na jambo hili?” Lakini tamko la mfalme lilikuwa na nguvu zaidi dhidi ya Yoabu na makamanda wa jeshi! Basi, Yoabu na makamanda wa jeshi wakaondoka mbele ya mfalme, wakaenda kuwahesabu Waisraeli. Walivuka mto Yordani wakianzia kuhesabu watu tangu Aroeri na mto ulioko bondeni kuelekea Gadi hadi Yazeri. Kisha, wakaenda Gileadi halafu Kadeshi katika nchi ya Wahiti, halafu wakawasili Dani na kutoka Dani wakazunguka kwenda Sidoni, na kufika kwenye ngome ya mji wa Tiro, wakaingia kwenye miji yote ya Wahivi na Wakanaani. Kisha, walitoka wakaenda Negebu ya Yuda huko Beer-sheba. Walipokwisha pitia katika nchi yote, walirejea Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini. Halafu Yoabu alimpelekea mfalme idadi ya watu. Katika Israeli kulikuwamo wanaume mashujaa 800,000 wenye ujuzi wa kutumia mapanga; na katika Yuda, kulikuwa na wanaume 500,000. Lakini Daudi alisumbuliwa sana rohoni mwake baada ya kuwahesabu watu. Kwa hiyo, Daudi akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa tendo nililolifanya. Lakini sasa, ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi unisamehe mimi mtumishi wako, kwani nimefanya jambo la kipumbavu kabisa.” Daudi alipoamka kesho yake asubuhi, wakati huo Mwenyezi-Mungu alimpa ujumbe nabii Gadi mwonaji wa mfalme Daudi, akisema, “Nenda ukamwambie hivi Daudi: ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Ninakupa mambo matatu, nawe ujichagulie mojawapo, nami nitakutendea.’” Hivyo, Gadi akamwendea Daudi na kumweleza, akisema, “Je, wapendelea njaa ya miaka saba iijie nchi yako? Au je, wewe uwakimbie adui zako kwa miezi mitatu wanapokufuatia? Au kuwe na siku tatu ambapo nchi yako itakuwa na maradhi mabaya? Fikiri unipe jibu nitakalompa yeye aliyenituma.” Daudi akamjibu Gadi, “Nina mashaka makubwa! Lakini afadhali niadhibiwe na Mwenyezi-Mungu, kuliko kutiwa mikononi mwa watu, maana yeye ana huruma sana.” Basi, Mwenyezi-Mungu akawaletea Waisraeli maradhi, tangu asubuhi hadi wakati uliopangwa. Watu 70,000 walikufa nchini kote kutoka Dani mpaka Beer-sheba. Lakini wakati malaika aliponyosha mkono wake kuelekea mji wa Yerusalemu ili kuuangamiza, Mwenyezi-Mungu alibadilisha nia yake. Mwenyezi-Mungu akamwambia huyo malaika aliyetekeleza maangamizi kwa watu, “Basi! Yatosha; rudisha mkono wako.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu alikuwa amesimama karibu na uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna, Myebusi. Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa anawaua watu, alimwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama, Mimi ndiye niliye na hatia! Mimi mwenyewe nimekosa! Hawa watu wapole hawakufanya uovu. Nakusihi sana uniadhibu mimi na jamaa ya baba yangu.” Siku hiyohiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, “Panda juu, ukamjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu, katika kiwanja cha kupuria nafaka cha Arauna, Myebusi.” Basi, Daudi akapanda juu kufuatana na neno la Gadi kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru. Arauna alipoangalia upande wa chini alimwona mfalme akimkaribia pamoja na watumishi wake, naye akatoka, akaenda na kumsujudia mfalme, akainama mpaka chini ardhini. Kisha Arauna akamwuliza mfalme, “Kwa nini bwana wangu mfalme amenijia mimi mtumishi wake?” Daudi akamjibu, “Nimekuja kununua uwanja wako wa kupuria nafaka ili nimjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu ili tauni iliyowakumba watu ikome.” Naye Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme, chukua chochote unachoona kinafaa na utolee sadaka. Mimi nawatoa fahali hawa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na vifaa hivi vya kupuria na nira za ng'ombe kuwa kuni. Hivi vyote, ee mfalme, nakupa. Natumaini Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atapokea sadaka yako kwa wema.” Lakini mfalme akamwambia Arauna, “La! Wewe hutanipa chochote. Mimi nitavinunua kwako kwa thamani yake. Sitamtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa ambazo hazijanigharimu kitu.” Hivyo, mfalme Daudi alinunua uwanja wa kupuria na fahali kwa fedha shekeli hamsini. Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu mahali hapo na kumtolea sadaka za kuteketezwa na za amani. Basi, Mwenyezi-Mungu akayakubali maombi kwa ajili ya nchi, na ile tauni iliyowakumba Waisraeli ikakoma. Mfalme Daudi, wakati alipokuwa mzee sana, watumishi wake walimfunika kwa mablanketi, lakini hata hivyo, hakuweza kupata joto. Kwa hivyo wakamwambia, “Bwana wetu mfalme, afadhali tukutafutie msichana akutumikie na kukutunza; alale pamoja nawe kusudi akupatie joto.” Basi, wakatafutatafuta msichana mzuri kote nchini Israeli. Akapatikana msichana mmoja mzuri aitwaye Abishagi, Mshunami; wakamleta kwa mfalme. Msichana huyo, alikuwa mzuri sana. Basi, akaanza kumtumikia na kumtunza mfalme; lakini mfalme hakulala naye. Wakati huo, Adoniya, mwana wa Daudi na Hagithi, akaanza kujigamba kwamba yeye ndiye atakayekuwa mfalme. Basi, akajitayarishia magari ya kukokotwa, wapandafarasi na wapiga mbio hamsini wa kumtangulia na kumshangilia. Lakini baba yake, Daudi, hakuwa amemkemea mwanawe hata mara moja na kumwuliza kwa nini alikuwa amefanya hivyo. Adoniya, ama kwa hakika, alikuwa mwenye sura ya kupendeza sana; na alikuwa amemfuata Absalomu kwa kuzaliwa. Adoniya akashauriana na Yoabu mwana wa Seruya, na kuhani Abiathari; nao wakamfuata na kumuunga mkono. Lakini kuhani Sadoki, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na nabii Nathani na Shimei, Rei pamoja na walinzi wa Daudi, hawakumuunga mkono Adoniya. Siku moja, Adoniya alitoa sadaka ya kondoo, ng'ombe na ndama wanono kwenye Jiwe la Nyoka, karibu na chemchemi iitwayo Enrogeli. Akawaalika kwenye karamu ya sadaka hiyo ndugu zake wote, yaani wana wengine wa mfalme, na watumishi wote wa mfalme waliokuwa wa kabila la Yuda. Lakini, nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Solomoni ndugu yake hakuwaalika. Hapo, Nathani akamwendea Bathsheba mama yake Solomoni, akamwuliza, “Je, hujasikia kwamba Adoniya, mwanawe Hagithi, amejinyakulia mamlaka ya ufalme na bwana wetu Daudi hana habari? Basi, kama ukitaka kuyaokoa maisha yako na ya mwanao Solomoni, nakushauri hivi: Mwendee mfalme Daudi, umwulize, ‘Je, bwana wangu mfalme, hukuniapia mimi mtumishi wako ukisema, “Mwana wako Solomoni atatawala mahali pangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?” Imekuwaje basi, sasa Adoniya anatawala?’ Na utakapokuwa bado unaongea na mfalme, mimi nitaingia na kuyathibitisha maneno yako.” Basi, Bathsheba alimwendea mfalme chumbani mwake (wakati huo mfalme alikuwa mzee sana, naye Abishagi, Mshunami alikuwa akimhudumia). Bathsheba aliinama, akamsujudia mfalme, naye mfalme akamwuliza, “Unataka nini?” Bathsheba akamjibu, “Bwana wangu, uliniapia mimi mtumishi wako mbele ya Bwana Mungu wako, ukisema: ‘Mwana wako Solomoni atatawala baada yangu, na ataketi juu ya kiti changu cha enzi.’ Sasa, tazama, Adoniya anatawala ingawa wewe bwana wangu mfalme hujui kuhusu hayo. Ametoa sadaka ya ng'ombe, ya vinono, na kondoo wengi, na kuwaita wana wote wa mfalme, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini mtumishi wako Solomoni hakumkaribisha. Na sasa, bwana wangu mfalme, Waisraeli wote wanakungojea, ili uwaambie yule atakayeketi juu ya kiti chako baada yako, bwana wangu mfalme. La sivyo, itatokea ya kwamba, wakati ambapo wewe bwana wangu, mfalme, utakapofariki mimi pamoja na mwanangu Solomoni tutahesabika kama wenye hatia.” Wakati Bathsheba alipokuwa akizungumza na mfalme, nabii Nathani aliingia ikulu. Nao watu wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Naye alipomfikia mfalme, alimwinamia mfalme mpaka uso ukafika chini udongoni. Ndipo Nathani aliposema, “Bwana wangu, je, ulisema, ‘Adoniya atatawala baada yangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?’ Kwa maana leo ameteremka, akatoa sadaka ya ng'ombe, vinono na kondoo wengi na amewakaribisha wana wa mfalme, Yoabu jemadari wa jeshi, na kuhani Abiathari, na, tazama, wanakula na kunywa mbele yake, na kusema, ‘Uishi mfalme Adoniya!’ Lakini hakunialika mimi, mtumishi wako wala kuhani Sadoki, wala Benaya mwana wa Yehoyada na mtumishi wako Solomoni. Je, yote haya umeyafanya wewe bwana wangu, mfalme, bila kuwaambia watumishi wako mtu atakayekaa juu ya kiti chako cha enzi baada yako?” Naye mfalme Daudi akajibu, “Niitie Bathsheba.” Bathsheba alimwendea mfalme na kusimama mbele yake. Halafu mfalme aliapa akisema, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, aliyekomboa roho yangu katika taabu nyingi, kama nilivyokuapia mbele za Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nikisema, ‘Mwanao Solomoni atatawala baada yangu, na kwamba atakaa juu ya kiti changu cha enzi badala yangu,’ ndivyo nitakavyofanya leo.” Ndipo Bathsheba alipoinama mpaka chini, akamsujudia mfalme, na kusema “Bwana wangu, mfalme Daudi, aishi milele!” Kisha mfalme Daudi akasema, “Niitie kuhani Sadoki, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada.” Nao wakamjia mfalme. Naye mfalme akawaambia, “Nenda na watumishi wangu mimi bwana wako, umpandishe mwanangu Solomoni juu ya nyumbu wangu, umpeleke Gihoni; halafu umruhusu kuhani Sadoki na nabii Nathani wampake mafuta kuwa mfalme wa Israeli; baadaye pigeni tarumbeta na kusema, ‘Mfalme Solomoni aishi!’ Nanyi mtamfuata, naye atakuja na kuketi juu ya kiti changu cha enzi badala yangu; nami nimemteua kuwa mtawala juu ya Israeli na juu ya Yuda.” Ndipo Benaya mwana wa Yehoyada alipomjibu mfalme, “Amina! Bwana Mungu wa bwana wangu mfalme, na anene vivyo hivyo. Kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa na bwana wangu mfalme, awe pia na Solomoni, na akikuze kiti chake cha enzi kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi.” Basi, kuhani Sadoki, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada, na Wakerethi na Wapelethi, wote walishuka wakampandisha Solomoni kwenye nyumbu wa mfalme Daudi, na kumpeleka mpaka Gihoni. Kisha kuhani Sadoki alichukua pembe za mafuta kutoka hemani na kumpaka mafuta Solomoni kuwa mfalme. Kisha walipiga tarumbeta; na watu wote wakasema, “Aishi mfalme Solomoni!” Halafu watu wote walimfuata, wakipiga mazomari, wakafurahi kwa shangwe kubwa, hata nchi ikatikisika kwa sauti zao. Basi, Adoniya pamoja na wageni waliokuwa naye walisikia hao watu walipomaliza sherehe. Naye Yoabu aliposikia sauti ya tarumbeta alisema, “Makelele hayo mjini ni ya nini?” Alipokuwa akisema, kumbe, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akaingia; kisha Adoniya akasema, “Karibu, kwani wewe u mtu mwema; unaleta habari njema.” Ndipo Yonathani alipomjibu Adoniya, “Hapana, kwa sababu mfalme Daudi amemtawaza Solomoni kuwa mfalme; naye mfalme amempeleka pamoja na kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada na Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme, kisha kuhani Sadoki na nabii Nathani wamemtia mafuta kuwa mfalme kule Gihoni; halafu wametoka hapo wakifurahi; ndicho kisa cha makelele hayo unayosikia. Sasa Solomoni anaketi juu ya kiti cha kifalme. Zaidi ya hayo, watumishi wa mfalme walikuja kumpongeza bwana wetu mfalme Daudi wakisema, ‘Mungu wako alifanye jina la Solomoni kuwa maarufu kuliko lako; pia akikuze kiti chake cha enzi kuliko kiti chako.’ Halafu mfalme akainama kitandani, na kuomba akisema, ‘Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, ambaye amemfanya mzawa wangu kuwa mfalme mahali pangu, na ambaye amenipa maisha hata nimeyaona haya.’” Basi, wageni wa Adoniya wakaogopa sana, wakaondoka na kutawanyika. Naye Adoniya, kwa kuwa alimwogopa Solomoni, akakimbilia katika hema la Mwenyezi-Mungu akazishika pembe za madhabahu apate kusalimika. Mfalme Solomoni akapata habari kwamba Adoniya alikuwa amekimbilia hemani, na kwamba anashikilia pembe za madhabahu akisema, “Sitaondoka hapa mpaka mfalme Solomoni atakaponihakikishia kwamba hataamuru niuawe.” Mfalme Solomoni akasema, “Nikimwona kuwa mwaminifu basi, hatapata madhara yoyote. Lakini nikimwona kuwa mwovu, lazima afe.” Basi, mfalme Solomoni akaagiza Adoniya aitwe kutoka hemani, aje kwake. Adoniya akafika mbele ya mfalme, akainama kwa heshima. Mfalme akamwambia, “Nenda zako nyumbani.” Daudi alipokaribia kufariki, alimwita mwanawe Solomoni, akampa wosia akisema, “Mwanangu, kama ilivyo kawaida kwa viumbe vyote kufa, siku zangu zimekwisha. Uwe imara na hodari. Timiza maagizo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ufuate njia zake na kushika masharti yake, amri zake, hukumu zake na kuheshimu maamuzi yake kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, ili upate kufanikiwa katika kila ufanyalo na kokote uendako, pia ili Mwenyezi-Mungu atimize ahadi yake aliyotoa aliponiambia kuwa, ikiwa wazawa wangu watatii amri zake na kumtumikia kwa uaminifu na kwa moyo wote, hakutakosekana mmoja wao kutawala Israeli nyakati zote. “Zaidi ya hayo, unajua pia yale aliyonitendea Yoabu, mwana wa Seruya; jinsi alivyowatendea majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua wakati wa amani akitaka kulipiza kisasi kwa mauaji waliyofanya wakati wa vita. Aliwaua watu wasiokuwa na hatia, nami nikachukua lawama kwa ajili ya vitendo vyake ambavyo vimeniletea mateso. Basi, wewe fanya kadiri ya hekima yako, ila tu usimwache afe kwa amani. “Lakini uwatendee mema wana wa Barzilai, Mgileadi, na uwatunze kwa ukarimu wawe kati ya wale wanaokula mezani pako; kwa sababu walinitendea mema wakati nilipomkimbia ndugu yako Absalomu. Pia, yupo Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini wa Bahurimu, ambaye aliniapiza na kunilaani vikali nilipokwenda Mahanaimu; lakini alipokuja kunilaki kwenye mto Yordani, nilimwapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu nikimwambia, ‘Sitakuua kwa upanga.’ Lakini wewe usimwache bila kumwadhibu. Wewe una hekima; utajua utakalomfanyia; ingawa yeye ana mvi, usimwache; muue ingawa ni mzee.” Daudi alifariki, akazikwa katika mji wake. Alikuwa ametawala Israeli kwa muda wa miaka arubaini; miaka saba akiwa Hebroni, na miaka thelathini na mitatu akiwa Yerusalemu. Basi, Solomoni akaketi katika kiti cha enzi mahali pa Daudi, baba yake; na ufalme wake ukaimarika. Baadaye, Adoniya mwana wa Hagithi, alimwendea Bathsheba, mama yake Solomoni. Bathsheba akamwuliza, “Je, unakuja kwa amani?” Adoniya akamjibu, “Ndiyo, nakuja kwa amani. Ila, nina jambo moja tu la kukuambia.” Bathsheba akamwambia, “Sema tu.” Adoniya akamwambia, “Unajua kwamba mimi ningalikuwa mfalme, na hata Israeli yote ilikuwa inanitazamia niwe mfalme. Lakini, mambo yakageuka na ndugu yangu akanipindua, kwani hayo ndio yaliyokuwa mapenzi yake Mwenyezi-Mungu. Sasa, ninalo ombi moja tu ambalo nakusihi usinikatalie.” Bathsheba akamwambia, “Sema tu.” Naye akasema, “Tafadhali, nakusihi umwombe mfalme Solomoni aniruhusu nimchukue Abishagi, yule Mshunami, awe mke wangu, kwa maana najua hatakukatalia wewe.” Bathsheba akamwambia, “Sawa; nitazungumza na mfalme kwa niaba yako.” Basi, Bathsheba akamwendea mfalme Solomoni kumweleza ombi la Adoniya. Mfalme akainuka kwenda kumlaki mama yake, akamwinamia. Halafu, akaketi katika kiti chake cha enzi, akaagiza mama yake aletewe kiti; naye akakaa upande wa kulia wa mfalme. Bathsheba akasema, “Nina ombi dogo tafadhali ulikubali, na ninakuomba usinikatalie.” Mfalme akamwambia, “Sema ombi lako mama yangu, kwa sababu sitakukatalia.” Naye akasema, “Mruhusu ndugu yako Adoniya amwoe Abishagi, huyo Mshunami.” Mfalme Solomoni akamwuliza mama yake, “Kwa nini unataka nimpe Abishagi? Hii ni sawa kabisa na kumtakia ufalme wangu! Kumbuka ya kwamba yeye ni kaka yangu mkubwa, na isitoshe, kuhani Abiathari na jemadari Yoabu mwana wa Seruya, wako upande wake!” Hapo mfalme Solomoni akaapa kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akisema, “Mungu na aniulie mbali ikiwa Adoniya hatakufa kwa sababu ya kutoa ombi hili! Sasa basi, kwa jina la Mwenyezi-Mungu aliye hai, aliyeniweka na kuniimarisha katika ufalme wa baba yangu Daudi, na aliyetimiza ahadi yake, akanipa enzi mimi na wazawa wangu, naapa kwamba hivi leo Adoniya atakufa!” Ndipo mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada; naye akamwendea Adoniya, akamuua. Mfalme Solomoni akamwambia kuhani Abiathari, “Ondoka uende shambani kwako, huko Anathothi; unastahili kufa wewe! Lakini sasa, sitakuua kwa sababu ulilishughulikia sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu ulipokuwa na baba yangu Daudi, ukateswa pamoja naye.” Basi, mfalme Solomoni akamfukuza Abiathari, asiwe kuhani wa Mwenyezi-Mungu; hivyo likatimia neno alilosema Mwenyezi-Mungu huko Shilo, juu ya Eli na ukoo wake. Yoabu alipopata habari, alikimbilia hemani mwa Mungu na kushikilia pembe za madhabahu; kwa maana alikuwa amemwunga mkono Adoniya na si Absalomu. Mfalme Solomoni aliposikia kwamba Yoabu yumo katika hema la Mungu na kwamba amesimama madhabahuni, alimtuma Benaya mwana wa Yehoyada, akisema, “Nenda ukampige.” Basi, Benaya akaenda katika hema la Mungu, akamwambia Yoabu, “Mfalme ameamuru utoke nje.” Yoabu akajibu, “Mimi sitoki; nitakufa papa hapa.” Benaya akarudi kwa mfalme na kumweleza alivyojibu Yoabu. Solomoni akasema, “Fanya alivyosema; umuue na kumzika. Hivyo, mimi na wazawa wengine wote wa Daudi hatutalaumiwa kwa vitendo vya Yoabu vya kuwaua watu wasio na hatia. Mungu atamwadhibu Yoabu kwa mauaji hayo aliyoyafanya bila baba yangu kuwa na habari. Yeye aliwaua watu wawili ambao walikuwa wa maana zaidi kuliko yeye, pia walimzidi kwa wema; aliwaua Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda. Adhabu ya mauaji hayo itakuwa juu ya Yoabu na wazawa wake milele. Bali Mwenyezi-Mungu atawapa ufanisi daima, Daudi na wazawa wake watakaokalia kiti chake cha enzi.” Basi, Benaya mwana wa Yehoyada, akaenda hemani, akamuua Yoabu ambaye alizikwa shambani mwake, nyikani. Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada, kuwa jemadari wa jeshi mahali pa Yoabu, na Sadoki akawa kuhani mahali pa Abiathari. Halafu mfalme akaagiza Shimei aitwe, akamwambia, “Jijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae hapa bila kwenda mahali pengine popote pale. Maana siku utakapotoka na kuvuka kijito Kidroni, nakuambia kweli utakufa, na kujilaumu wewe mwenyewe kwa kifo chako.” Shimei akajibu, “Vema mfalme. Nitafanya kama ulivyosema.” Basi, akakaa Yerusalemu muda mrefu. Lakini mwishoni mwa mwaka wa tatu, watumwa wawili wa Shimei walitoroka, wakaenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Habari zilipomfikia kwamba wako Gathi, Shimei alipanda punda wake, akaenda huko kuwatafuta, kwa mfalme Akishi. Basi, akafika, akawapata, akawarudisha nyumbani. Mfalme Solomoni alipopata habari kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu, akaenda Gathi na kurudi, alimwita Shimei na kumwambia, “Je, hukuniapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu kwamba hutatoka Yerusalemu, nami sikukuonya kwa dhati kwamba, hakika utakufa kama utathubutu kwenda nje? Nawe ulikubali, ukaniambia, ‘Vema, nitatii.’ Mbona basi, umevunja kiapo chako kwa Mwenyezi-Mungu na kutojali amri niliyokupa?” Mfalme aliendelea kumwambia Shimei, “Unayajua wazi maovu uliyomtendea baba yangu Daudi, na sasa, kwa sababu ya hayo, Mwenyezi-Mungu atakuadhibu. Lakini mimi atanibariki, na kiti cha enzi cha Daudi kitaimarishwa mbele ya Mwenyezi-Mungu milele.” Hapo, mfalme akamwamuru Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka, akampiga na kumuua Shimei. Basi, ufalme ukaimarika chini ya Solomoni. Solomoni alifanya ushirikiano na Farao mfalme wa Misri, kwa kumwoa binti yake. Akamleta binti Farao na kumweka katika mji wa Daudi, mpaka alipomaliza kujenga nyumba yake mwenyewe, nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na ukuta wa kuuzunguka mji wa Yerusalemu. Kabla yake, watu walikuwa wakitoa tambiko vilimani, kwa kuwa nyumba ya Mungu ilikuwa bado haijajengwa. Solomoni alimpenda Mwenyezi-Mungu, akazingatia maongozi ya Daudi, baba yake; ila tu, naye ilimbidi kutoa tambiko na kufukiza ubani vilimani. Wakati mmoja, Solomoni alikwenda kutoa tambiko huko Gibeoni, maana palikuwa ndipo mahali maarufu pa ibada. Ilikuwa ni kawaida ya Solomoni kutoa maelfu ya sadaka za kuteketezwa katika madhabahu hiyo. Huko Gibeoni, Mwenyezi-Mungu alimtokea Solomoni katika ndoto usiku, akamwambia, “Omba chochote nami nitakupa.” Solomoni akamwambia, “Ulimwonesha mtumishi wako Daudi, baba yangu, fadhili nyingi, kwa sababu alikutumikia kwa uaminifu, uadilifu na kwa haki; na umedumisha fadhili zako kwa kumpa mwana anayeketi sasa kwenye kiti chake cha enzi. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umeniweka mimi mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, ijapokuwa ningali mtoto mdogo na sijui namna ya kutekeleza wajibu huu. Na hapa umeniweka kati ya watu wako ambao umewachagua; nao ni wengi hata hawawezi kuhesabika kwa wingi wao. Kwa hiyo, nakuomba unipe mimi mtumishi wako moyo wa kusikia ili kuamua watu wako, niweze kutambua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuhukumu watu wako walio wengi hivi?” Ombi hili la Solomoni lilimfurahisha Mwenyezi-Mungu, naye akamwambia, “Kwa kuwa umetoa ombi hili, na hukujiombea maisha marefu au mali, na wala hukuomba adui zako waangamizwe, bali umejiombea utambuzi wa kutoa hukumu au kutenda haki basi, sasa nakutimizia kama ulivyoomba. Tazama, nakupa hekima na akili kiasi ambacho hapana mtu mwingine aliyepata kuwa nacho kabla yako, na wala hatatokea mwingine kama wewe baada yako. Pia, nitakupa yale ambayo hukuomba: Nitakupa utajiri na heshima zaidi ya mfalme mwingine yeyote wa nyakati zako. Tena kama ukifuata njia na maagizo yangu na kushika amri zangu kama alivyofanya baba yako Daudi, basi, nitakupa maisha marefu.” Solomoni alipoamka, alitambua kwamba ilikuwa ndoto. Ndipo akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, akamtolea tambiko za kuteketezwa na za amani. Halafu akawafanyia karamu watumishi wake wote. Siku moja, wanawake wawili makahaba, walikwenda kwa mfalme Solomoni. Mmoja wao akasema, “Ee bwana wangu, mimi na huyu mwenzangu tunakaa nyumba moja; mimi nilijifungua mtoto wakati huyu dada yumo nyumbani. Siku tatu baadaye, huyu naye alijifungua mtoto. Hapakuwa na mtu mwingine nyumbani ila sisi wawili tu. Halafu, usiku mmoja, mtoto wake alifariki kwa sababu alimlalia. Kisha akaamka usiku wa manane, akamchukua mwanangu kutoka kwangu wakati mimi nipo usingizini, akamlaza kifuani pake. Halafu akaichukua maiti ya mwanawe, akailaza kifuani pangu. Nilipoamka asubuhi na kutaka kumnyonyesha mwanangu, nikakuta mtoto amefariki. Nilipochunguza sana, nikagundua kuwa hakuwa mwanangu niliyemzaa.” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Wa kwangu ndiye aliye hai na wa kwako ndiye aliyekufa”. Naye mwanamke wa kwanza akasema, “La! Mtoto wako ndiye aliyekufa, wangu ni huyo aliye hai!” Basi, wakaendelea kubishana hivyo mbele ya mfalme. Ndipo mfalme Solomoni akasema, “Kila mmoja wenu anadai kwamba, mtoto wake ndiye aliye hai na kwamba aliyekufa si wake.” Basi, mfalme akaagiza: “Nileteeni upanga!” Wakamletea mfalme upanga. Mfalme akasema: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, umpe mmoja nusu na mwingine nusu.” Yule mwanamke aliyekuwa mama yake huyo mtoto aliye hai alishikwa na huruma juu ya mwanawe, akamwambia mfalme, “Tafadhali mfalme, msimuue mtoto. Mpe mwenzangu huyo mtoto aliye hai, amchukue yeye.” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “La! Mtoto asiwe wangu wala wake. Mkate vipande viwili.” Mfalme Solomoni akasema, “Usimuue mtoto! Mpe mwanamke wa kwanza amchukue, kwani yeye ndiye mama yake.” Watu wote wa Israeli waliposikia juu ya hukumu ya mfalme, walimwogopa, wakatambua kwamba alikuwa na hekima ya Mungu iliyomwezesha kutoa hukumu. Solomoni alikuwa mfalme wa nchi yote ya Israeli, na wafuatao walikuwa baadhi ya maofisa wake wa vyeo vya juu: Azaria, mwana wa Sadoki, alikuwa kuhani. Elihorefu na Ahiya wana wa Shausha, walikuwa makatibu; Yehoshafati mwana wa Ahiludi, alikuwa mweka kumbukumbu za habari. Benaya mwana wa Yehoyada, alikuwa jemadari wa jeshi; nao Sadoki na Abiathari, walikuwa makuhani. Azaria mwana wa Nathani, alikuwa ofisa mkuu tawala; kuhani Zabudi mwana wa Nathani, alikuwa rafiki wa mfalme. Ahishari alikuwa mkuu wa ikulu na Adoniramu mwana wa Abda, alikuwa msimamizi wa kazi za kulazimishwa. Solomoni aliteua maofisa tawala kumi na wawili kwa nchi nzima ya Israeli. Hao walipewa jukumu la kutafuta chakula kwa ajili ya mfalme na nyumba yake; kila mmoja wao alileta chakula kutoka mkoani kwake kwa mwezi mmoja kila mwaka. Haya ndiyo majina ya hao maofisa tawala: Ben-huri alisimamia sehemu ya milima ya Efraimu; Ben-dekeri alisimamia miji ya Makai, Shaalbimu, Beth-shemeshi na Elon-beth-hanani. Ben-hesedi alisimamia mji wa Arubothi, alisimamia pia Soko na nchi yote ya Heferi. Ben-abinadabu, mume wa Tafathi, binti Solomoni, alisimamia kanda yote ya Nafath-dori. Baana, mwana wa Ahiludi, alisimamia miji ya Taanaki, Megido, na sehemu yote ya Beth-sheani iliyo karibu na mji wa Zarethi, kusini ya mji wa Yezreeli, na kutoka Beth-sheani mpaka miji ya Abel-mehola, na hata kupita mji wa Yokmeamu. Ben-geberi, alisimamia mji wa Ramoth-gileadi pamoja na vijiji vya Gileadi vilivyokuwa chini ya Yairi, mwana wa Manase; pia alisimamia mkoa wa Argobu ulioko Bashani; yote jumla ilikuwa miji mikubwa sitini iliyozungushiwa kuta na kuwekwa fito za shaba malangoni. Ahinadabu, mwana wa Ido, alisimamia jimbo la Mahanaimu. Ahimaasi, mumewe Basemathi, binti Solomoni, alisimamia wilaya ya Naftali. Baana mwana wa Hushai, alisimamia wilaya ya Asheri na Bealothi. Yehoshafati mwana wa Parua, alisimamia wilaya ya Isakari. Shimei, mwana wa Ela, alisimamia wilaya ya Benyamini. Geberi, mwana wa Uri, alisimamia wilaya ya Gileadi, ambayo hapo awali ilitwaliwa na Sihoni mfalme wa Waamori, na Ogu mfalme wa Bashani. Licha ya hawa kumi na wawili, palikuwa na mkuu mmoja aliyesimamia nchi nzima ya Yuda. Watu wa Yuda na wa Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani, nao walikuwa wakila, wakinywa, na kufurahi. Solomoni alitawala falme zote kuanzia mto Eufrate mpaka nchi ya Wafilisti, hadi mpakani na Misri. Mataifa yote yalimtumikia na kulipa kodi kwake wakati wote wa maisha yake. Chakula alichohitaji Solomoni kwa siku moja, kilikuwa unga laini madebe 360, na unga wa kawaida madebe 720, ng'ombe wanono kumi, na ng'ombe wa kundini ishirini, kondoo 100 pamoja na kulungu, paa, swala na kuku wanono. Naam, nchi yote magharibi ya mto Eufrate: Kutoka Tifsa mpaka mji wa Gaza, ilikuwa chini ya utawala wake. Wafalme wote magharibi ya mto Eufrate walikuwa chini yake, na alikuwa na amani na nchi zote jirani. Siku zote za utawala wake Solomoni, watu wa Yuda na watu wa Israeli, toka Dani mpaka Beer-sheba, walikaa salama, kila mtu kwenye miti yake ya mizabibu na mitini. Solomoni alikuwa na vibanda 40,000 kwa ajili ya farasi wa magari yake ya kukokotwa, na askari wapandafarasi 12,000. Wale maofisa wake kumi na wawili, kila mmoja kwa mwezi aliopangiwa, walipeleka chakula cha kutosha kwa ajili ya mfalme na wale wote waliokula nyumbani mwake. Mahitaji yao yote yalitoshelezwa. Zamu ya kila mmoja ilipofika, alipeleka pia shayiri na majani ya kulisha farasi na wanyama waendao kasi. Mungu alimpa Solomoni hekima zaidi na akili kwa wingi; maarifa yake yalikuwa kama mchanga wa pwani, hayakuwa na kipimo. Hekima ya Solomoni iliipita hekima ya watu wa mashariki na iliishinda hekima ya watu wa Misri. Aliwashinda watu wote kwa hekima; aliwashinda Ethani, yule Mwezrahi, Hemani na Kalkoli na Darda, wana wa Maholi; na sifa zake zilienea katika mataifa yote jirani. Alitunga methali 3,000 na nyimbo 1,500. Alizungumza habari za miti, kuanzia mwerezi ulioko Lebanoni, hata husopo, mmea uotao ukutani. Alizungumza pia juu ya wanyama, ndege, jamii ya wanyama wenye damu baridi watagao mayai, na juu ya samaki. Watu kutoka mataifa yote, na wafalme wote waliopata kusikia habari kuhusu hekima yake, walikuja kumsikiliza. Naye mfalme Hiramu wa Tiro, aliyekuwa rafiki ya Daudi, alipopata habari kwamba Solomoni amekuwa mfalme mahali pa baba yake, alituma watumishi kwake. Ndipo Solomoni akampelekea Hiramu ujumbe huu: “Wajua kwamba baba yangu Daudi hakuweza kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, hekalu la kumwabudia, kwa sababu ya kukumbana na vita vingi dhidi ya maadui wa nchi jirani mpaka hapo Mwenyezi-Mungu alipompatia ushindi. Lakini sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, amenijalia amani pande zote. Sina adui wala taabu. Basi, nimeamua kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nyumba ya kumwabudia. Na hii ni sawa kabisa kama Mwenyezi-Mungu alivyomwahidi baba yangu akisema: ‘Mwanao ambaye nitamfanya aketi katika kiti chako cha enzi, atanijengea nyumba!’ Sasa basi, uwaamuru watu wako wanikatie mierezi ya Lebanoni. Watu wangu watajiunga na watu wako katika kazi hiyo, nami nitawalipa watumishi wako kadiri utakavyosema; kwani kama ujuavyo, hakuna yeyote mwenye ujuzi wa kukata miti kama nyinyi Wasidoni.” Hiramu alifurahi sana alipopata ujumbe huu wa Solomoni, akasema, “Mwenyezi-Mungu asifiwe wakati huu, kwa kumpa Daudi mwana mwenye hekima atawale taifa hili kubwa.” Kisha, Hiramu alimpelekea Solomoni ujumbe, akisema, “Nimepokea ujumbe wako, nami niko tayari kutimiza mahitaji yako kuhusu mbao za mierezi na za miberoshi. Watu wangu watasomba magogo na kuyateremsha kutoka Lebanoni mpaka baharini na kuyafunga mafungumafungu yaelee juu ya maji mpaka mahali utakaponielekeza. Huko, yatafunguliwa, nawe utayapokea. Kwa upande wako, wewe utanipa chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwangu.” Basi, Hiramu alimpa Solomoni mbao zote za aina ya mierezi na miberoshi alizohitaji, naye Solomoni akampa Hiramu ngano madebe 240,000, na mafuta safi madebe 200 kila mwaka, kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake. Basi, Mwenyezi-Mungu akampa Solomoni hekima kama alivyomwahidi. Kukawa na amani kati ya Solomoni na Hiramu; wakafanya mkataba kati yao. Mfalme Solomoni alikusanya watu 30,000 kutoka kila mahali nchini Israeli, wafanye kazi za kulazimishwa, akamweka Adoniramu awe msimamizi wao. Aliwagawa watu hao katika makundi matatu ya watu 10,000 kila moja, akayapeleka makundi hayo kwa zamu, mwezi mmoja Lebanoni na miezi miwili nyumbani. Solomoni alikuwa pia na wachukuzi wa mizigo 70,000, na wachongaji mawe milimani 80,000, mbali na maofisa wakuu 3,300 waliosimamia kazi hiyo na wafanyakazi wote. Kwa amri ya mfalme, walichimbua mawe makubwa na ya thamani, ili yachongwe kwa ajili ya kujengea msingi wa nyumba. Basi, hivyo ndivyo wajenzi wa Solomoni na Hiramu na watu wa mji wa Gebali walivyotayarisha mawe na mbao za kujengea nyumba hiyo. Solomoni alianza kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu katika mwaka wa 480 baada ya Waisraeli kutoka Misri. Huo ulikuwa mwaka wa nne wa utawala wa Solomoni juu ya Israeli, katika mwezi wa Zifu, yaani mwezi wa pili. Nyumba hiyo ambayo mfalme Solomoni alimjengea Mwenyezi-Mungu ilikuwa na urefu wa mita 27, upana wa mita 9, na kimo cha mita 13.5. Ukumbi wa sebule ya nyumba ulikuwa na upana wa mita 4.5 toka upande mmoja wa nyumba mpaka upande mwingine. Na kina chake mbele ya hiyo nyumba kilikuwa mita 9. Aliiwekea nyumba hiyo madirisha mapana kwa ndani na membamba kwa nje. Pia alijenga nguzo kuzunguka, ili kutegemeza ukuta wa nje; akatengeneza na vyumba vya pembeni kila upande. Vyumba vya chini, katika hivyo vyumba vya nyongeza, vilikuwa na upana wa mita 2.25, na ghorofa iliyofuata ilikuwa na upana wa mita 2.75, na ghorofa ya juu kabisa ilikuwa na upana wa mita 3. Ghorofa hizo zilikuwa zimetofautiana kwa upana, kwa sababu Solomoni alikuwa amepunguza kiasi ukuta wa nje kuzunguka nyumba, ili boriti za kutegemeza jengo zisishikamane na kuta. Wakati nyumba ilipokuwa inajengwa, hapakusikika ndani ya nyumba mlio wa nyundo, wala wa chombo chochote cha chuma, maana ilijengwa kwa mawe yaliyokuwa yamechongwa na kutayarishwa kabisa huko yalikochukuliwa. Mlango wa kuingilia sehemu ya chini ya jengo lililoongezwa ubavuni mwa nyumba, ulikuwa upande wa kusini. Ndani, mlikuwa na ngazi ambayo watu waliweza kupanda ili kwenda ghorofa ya katikati na ya mwisho. Hivyo, Solomoni aliijenga nyumba, ikamalizika. Dari ya nyumba alikuwa ameitengeneza kwa boriti na mbao za mierezi. Kuuzunguka ukuta wa nje wa nyumba hiyo, alijenga vyumba vya ghorofa vyenye kimo cha mita 2.25; navyo vilikuwa vimeunganishwa na nyumba kwa boriti za mierezi. Wakati huo, ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu ukamjia Solomoni, “Kuhusu nyumba hii unayoijenga, kama ukifuata maongozi yangu, ukayatii maagizo yangu na amri zangu, nitakutimizia mambo yote niliyomwahidi baba yako Daudi. Mimi nitakaa miongoni mwa wazawa wa Israeli, na sitawaacha kamwe watu wangu, Israeli.” Hivyo, Solomoni akaijenga nyumba na kuimaliza. Upande wa ndani wa kuta za nyumba aliufunika kwa mbao za mierezi, kutoka sakafuni mpaka kwenye boriti za dari; na sakafu akaitandika mbao za miberoshi. Chumba cha ndani, kilichoitwa mahali patakatifu sana, kilijengwa katika sehemu ya nyuma ya nyumba. Kilikuwa kimejengwa kwa mbao za mierezi kutoka sakafuni hadi darini, na urefu wake ulikuwa mita 9. Nyumba ile iliyokuwa mbele ya mahali patakatifu sana, ilikuwa na urefu wa mita 18. Mbao za mierezi zilizotanda ukuta wa nyumba kwa ndani zilikuwa zimepambwa kwa michoro ya mibuyu na maua yaliyochanua. Kila sehemu ilikuwa imefunikwa kwa mbao za mierezi, wala hapana jiwe lililoonekana. Katika sehemu ya ndani kabisa ya jengo hilo, Solomoni alitayarisha chumba cha pekee ambamo sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwekwa. Chumba hicho kilikuwa na urefu wa mita 9, upana wa mita 9, na kimo cha mita 9; nacho kilipambwa kwa dhahabu safi. Pia, alitengeneza madhabahu kwa mbao za mierezi. Solomoni aliipamba kwa dhahabu safi sehemu ya ndani ya nyumba, na mbele ya hicho chumba cha ndani akaweka minyororo ya dhahabu kutoka upande mmoja mpaka upande wa pili, aliipamba kwa dhahabu. Nyumba yote aliipamba kwa dhahabu, na madhabahu iliyokuwa katika chumba cha ndani kabisa. Alitengeneza kwa mbao za mizeituni sanamu za viumbe wawili wenye mabawa, kila sanamu ikiwa na kimo cha mita 4.5, akaziweka katika chumba cha ndani kabisa. Kila bawa lilikuwa na urefu wa mita 2.5; kwa hiyo urefu kutoka ncha ya bawa moja mpaka ncha ya bawa lingine ulikuwa mita 4.5. Kiumbe mwingine alikuwa na urefu wa mita 4.5; viumbe wote wawili walikuwa na vipimo vilevile na umbo lilelile. Urefu wa kiumbe mmoja ulikuwa mita 4.5; pia urefu wa kiumbe mwingine ulikuwa uleule. Sanamu hizo zilikuwa sambamba, zikiwa na mabawa yaliyokunjuliwa: Bawa la mmoja likigusa ukuta mmoja, na bawa la mwingine likigusa ukuta wa pili, huku yale mengine yaligusana katikati ya chumba. Nazo sanamu hizo alizipamba kwa dhahabu. Kuta za kila chumba alizipamba kwa kuchongwa michoro ya viumbe wenye mabawa, mitende na michoro ya maua yaliyochanua. Aliipaka dhahabu sakafu ya vyumba vya ndani na vya nje. Kwa kuingia chumba cha ndani kabisa alitengeneza milango kwa mbao za mizeituni. Vizingiti na miimo ya milango vilifanya umbo la pembe tano. Katika milango hiyo miwili ya mizeituni, alichora viumbe wenye mabawa, mitende na maua yaliyochanua; akaipamba michoro hiyo kwa dhahabu. Hali kadhalika, alitengeneza mlango wa mraba wa kuingia sebuleni. Miimo ya mlango huo ilikuwa ya mizeituni, na mabamba yake mawili yalikuwa ya miberoshi; kila bamba liliweza kukunjwa mara moja. Juu ya mabamba hayo ya mlango, kulichorwa viumbe wenye mabawa, mitende na maua yaliyochanua; akaipamba vizuri michoro hiyo kwa dhahabu. Alijenga ukumbi wa ndani ambao kuta zake zilikuwa za tabaka tatu za mawe yaliyochongwa, na tabaka moja la boriti za mwerezi. Msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu ulijengwa mnamo mwezi wa Zifu katika mwaka wa nne. Na katika mwezi wa Buli, yaani mwezi wa nane, katika mwaka wa kumi na mmoja, ujenzi wa nyumba ulimalizika, na kazi ilikuwa imekamilika kama ilivyopangwa. Ujenzi huo ulimchukua Solomoni miaka saba. Solomoni alijijengea ikulu, nayo ilimchukua miaka kumi na mitatu kumalizika. Kisha, akajenga jengo lililoitwa Nyumba ya Msitu wa Lebanoni. Urefu wake ulikuwa mita 44.5, upana wake mita 22.25, na kimo chake mita 13.5. Ilikuwa imejengwa juu ya safu 3 za nguzo za mierezi, nguzo ambazo zilishikilia boriti za mierezi kwa upande wa juu. Kila safu ilikuwa na nguzo 15; basi zote pamoja zilikuwa nguzo 45. Vyumba vilivyojengwa juu ya nguzo hizo, alivitilia dari ya mbao za mierezi. Kulikuwa na safu tatu za madirisha yaliyoelekeana. Milango yote ilikuwa ya mraba, na miimo ya madirisha hayo yaliyoelekeana ilikuwa pia ya mraba. Alijenga ukumbi wa nguzo, ambao urefu wake ulikuwa mita 22.25, na upana wake mita 13.5. Kwenye sehemu ya mbele ya jengo hilo kulikuwa na sebule. Mbele ya sebule kulikuwa na nguzo; na mbele ya nguzo kulitokeza paa dogo. Solomoni alijenga ukumbi wa kiti cha enzi ambamo aliamulia kesi za watu. Huu uliitwa pia Ukumbi wa Hukumu. Ulikuwa umepambwa kwa mbao za mierezi kutoka sakafu mpaka dari. Nyumba yake ya kukaa mwenyewe, iliyokuwa nyuma ya Ukumbi wa Hukumu, ilikuwa imejengwa kama zile nyingine. Solomoni pia alijenga nyumba kama ukumbi huo kwa ajili ya binti Farao, ambaye alikuwa amemwoa. Majengo hayo yote yalijengwa kwa mawe ya thamani kutoka msingi mpaka juu, mawe ambayo yalikuwa yamechongwa kwa vipimo maalumu, na kukatwa kwa msumeno upande wa ndani na wa nje. Msingi ulikuwa wa mawe ya thamani na makubwa yenye urefu wa mita 3.5, na upana mita 4.5. Sehemu za juu zilijengwa kwa mawe mengine yaliyochongwa kwa vipimo maalumu, na kwa mbao za mierezi. Ua wa nyumba ya mfalme ulikuwa na kuta zenye safu moja ya mbao za mierezi na safu tatu za mawe ya kuchongwa kila moja; ndivyo ilivyokuwa hata kwa ua wa ndani wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kwa ukumbi wa nyumba. Kisha mfalme Solomoni alimwita Hiramu kutoka Tiro. Huyo, alikuwa mwana wa mjane wa kabila la Naftali, na baba yake alikuwa mkazi wa Tiro, mfua shaba. Hiramu alikuwa na hekima nyingi na akili, na fundi stadi wa kazi yoyote ya shaba. Basi, alikuja kwa mfalme Solomoni, akamfanyia kazi yake yote. Hiramu alitengeneza nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa mita 54, na mzingo wa mita 5.5. Ndani zilikuwa na tundu ambalo unene wa pande zake ulikuwa sentimita 2. Akatengeneza pia taji mbili za shaba, kila moja ikiwa na kimo cha mita 2.25; akaziweka juu ya nguzo hizo. Halafu, alifuma nyavu mbili zenye mapambo ya mrabamraba, akatengeneza na taji kwa kusokota mkufu: Vyote hivyo kwa ajili ya kupamba taji za shaba zilizowekwa juu ya zile nguzo. Hali kadhalika, alitengeneza matunda aina ya makomamanga, akayapanga safu mbili kuzunguka zile taji juu ya kila nguzo. Na taji hizo zilizokuwa juu ya nguzo mbele ya sebule, zilipambwa kwa mifano ya maua ya yungiyungi, kimo chake mita 1.75. Taji hizo zilikuwa juu ya hizo nguzo mbili, na pia zilikuwa juu ya sehemu ya mviringo iliyojitokeza karibu na zile nyavu. Palikuwa na mifano 400 ya matunda ya mkomamanga, imepangwa safu mbili kuzunguka kila taji. Hiramu aliziweka nguzo hizo kwenye sebule ya hekalu; nguzo aliyoisimika upande wa kusini iliitwa Yakini, na ile aliyoisimika upande wa kaskazini iliitwa Boazi. Vichwa vya nguzo hizo vilipambwa kwa mfano wa maua ya yungiyungi. Na hivyo kazi ya kutengeneza nguzo ikamalizika. Hiramu alitengeneza Birika liitwalo Bahari. Lilikuwa la mviringo lenye upana wa mita 4.5 kutoka ukingo hadi ukingo, na urefu wa mita 2.25 na mzingo wa mita 13.5. Chini ya ukingo wake, kulizunguka tangi hilo, kulikuwa na safu mbili za vibuyu, kila kimoja mita 13.5. Vibuyu hivyo vilikuwa vimetengenezwa wakati huohuo tangi hilo lilipofanywa. Nalo tangi lilikuwa limewekwa juu ya sanamu za mafahali kumi na wawili; tatu zikielekea upande wa kaskazini, tatu zikielekea magharibi, tatu kusini, na nyingine tatu mashariki. Tangi liliwekwa juu ya mafahali hao, sehemu zao za nyuma zikiwa ndani. Unene wa ukingo wake ulikuwa sentimita 7.5; nao ulikuwa ukifanana na ukingo wa kikombe na kama ua la yungiyungi. Tangi liliweza kujaa maji kiasi cha lita 40,000. Hiramu pia alitengeneza magari kumi ya shaba, kila gari likiwa na urefu wa mita 1.75, upana wa mita 1.75, na kimo cha mita 1.25. Magari hayo yalikuwa yameundwa hivi: Kulikuwa na mabamba ya chuma ambayo yalikuwa yameshikiliwa na mitalimbo. Juu ya mabamba hayo yaliyoshikiliwa na mitalimbo, kulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe wenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali, zilikuwa zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuri. Isitoshe, kila gari lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya katikati vya kuyazungukia magurudumu hayo, vilikuwa vya shaba. Kwenye pembe nne za gari kulikuwa na vishikizo vya shaba kwa ajili ya birika kubwa. Karibu ya kila kishikio kuliwekwa mapambo ya maua ya kusokotwa. Mlango wa gari ulikuwa katika sehemu iliyotokeza juu kwa kiasi cha nusu mita. Kwa nje, mlango ulikuwa umetiwa michoro; na mabamba yake yalikuwa ya mraba, si ya mviringo. Na hayo magurudumu manne yalikuwa chini ya yale mabamba; vyuma vya katikati kuzunguka magurudumu hayo vilikuwa vimeunganishwa na mfumo wa gari lenyewe; na kimo cha magurudumu hayo kilikuwa sentimita 66. Hayo magurudumu yalikuwa kama magurudumu ya magari ya kukokotwa; na vyuma vyake vya katikati, duara zake, mataruma yake na vikombe vyake: Hivyo vyote vilikuwa vya kusubu. Chini ya kila gari kulikuwa na mihimili minne kwenye pembe zake, nayo ilishikamanishwa na gari. Na juu ya kila gari palikuwa na utepe uliofanyiza duara ya kimo cha sentimita 22; na vishikio na mabamba yaliyokuwa upande wa juu yalishikamana na gari lenyewe. Kwenye nafasi wazi iliyopatikana katika vishikio na mabamba ya kila gari, Hiramu alichonga michoro ya viumbe wenye mabawa, simba na miti ya mitende, akazungushia na mashada ya mapambo. Mifano hiyo yote kumi ya magari ilifanana, ikiwa na kimo kimoja na muundo uleule. Hiramu, pia alitengeneza mabirika kumi ya shaba, moja kwa kila gari. Kila birika ilikuwa na upana wa mita 1.75, na iliweza kuchukua maji kadiri ya lita 880. Akaweka magari matano upande wa kusini wa nyumba, na matano upande wa kaskazini; na lile tangi akaliweka kwenye pembe ya kusini-mashariki ya nyumba. Hiramu alitengeneza pia vyungu, sepetu na mabirika. Basi, Hiramu akamaliza kazi aliyoamriwa na mfalme Solomoni kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Nguzo mbili, mabakuli mawili ya taji zilizowekwa juu ya nguzo, na nyavu mbili kwa ajili ya kufunika hizo taji mbili, mifano ya makomamanga 400 kwa ajili ya nyavu hizo mbili, safu mbili za makomamanga kwa kila wavu ili kupamba zile taji mbili zilizokuwa juu ya nguzo. Hali kadhalika, alitengeneza magari kumi, na vishikio kumi katika magari hayo; na tangi lile moja na sanamu za mafahali kumi na wawili, chini ya hilo tangi. Halafu vile vyungu, sepetu na mabirika, vyombo hivyo vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambavyo Hiramu alimtengenezea mfalme Solomoni, vilikuwa vya shaba iliyongarishwa. Vitu hivyo vyote mfalme alivitengeneza katika uwanda wa Yordani, sehemu ya udongo wa mfinyanzi iliyokuwa kati ya Sukothi na Sarethani. Solomoni hakupima uzani wa vifaa hivi vyote kwa kuwa vilikuwa vingi sana, na kwa sababu uzani wa shaba haukujulikana. Solomoni alitengeneza vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Madhabahu ya dhahabu, meza ya dhahabu kwa ajili ya mikate ya kuwekwa mbele ya Mungu, vinara vya taa vya dhahabu safi vilivyowekwa mbele ya mahali patakatifu sana, vitano upande wa kusini na vitano upande wa kaskazini; maua, taa, koleo, vyote vikiwa vya dhahabu; vikombe, makasi ya kukatia tambi za mishumaa, mabakuli, vyetezo vya kuwekea ubani, miiko ya kuchukulia moto, vyote vya dhahabu safi; bawaba za milango ya sehemu ya ndani kabisa ya nyumba — pale mahali patakatifu sana — na bawaba za milango ya ukumbi wa ibada wa hekalu bawaba zote za dhahabu. Basi, mfalme Solomoni akamaliza kazi zote zilizohusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kisha Solomoni akaleta mali yote ambayo baba yake Daudi, alikuwa ameiweka wakfu, yaani: Fedha, dhahabu na vyombo; akaiweka katika hazina za nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Basi, mfalme Solomoni akawakutanisha mbele yake huko Yerusalemu wazee na viongozi wote wa makabila na wa koo za Israeli ili waliondoe sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu katika mji wa Daudi, yaani Siyoni. Wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, yaani mwezi wa saba. Ndipo watu hao wote walipokusanyika mbele ya mfalme Solomoni. Baada ya wazee wote wa Israeli kuwasili, makuhani walibeba sanduku la agano. Walawi na makuhani walihamisha sanduku la agano na hema la mkutano, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa humo hemani. Mfalme Solomoni na mkutano wote wa Israeli wakakusanyika mbele ya sanduku la agano, nao wakatoa tambiko: Ng'ombe na kondoo wasiohesabika. Kisha makuhani wakaliingiza sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu mahali pake, katika chumba cha ndani cha nyumba mahali patakatifu sana, chini ya mabawa ya viumbe wenye mabawa. Hao viumbe wenye mabawa walitandaza mabawa yao juu ya mahali lilipowekwa sanduku, kwa hiyo sanduku na mipiko yake ya kulibebea vilikuwa chini ya mabawa. Kwa kuwa mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana, ncha zake ziliweza kuonekana kutoka mahali patakatifu, mbele ya chumba cha ndani; lakini haikuweza kuonekana kutoka upande wa nje. Mipiko hiyo ingali mahali hapo hata leo. Hapakuwa na kitu ndani ya sanduku la agano ila vile vibao viwili vya mawe ambavyo Mose aliviweka humo kule Horebu, mahali Mwenyezi-Mungu alipofanya agano na Waisraeli walipotoka nchini Misri. Ikawa, makuhani walipotoka pale mahali patakatifu, wingu liliijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani walishindwa kuhudumu kwa sababu ya wingu hilo; kwa kuwa utukufu wa Mwenyezi-Mungu uliijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Ndipo Solomoni akasema, “Mwenyezi-Mungu alisema kwamba, atakaa katika giza nene. Hakika, nimekujengea nyumba ya kukaa, mahali pa makao yako ya milele.” Kisha, Solomoni akaigeukia jumuiya yote ya Waisraeli wakiwa wamesimama, akawabariki, akasema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwani kwa nguvu yake ametimiza ahadi yake aliyompa baba yangu Daudi, akisema: ‘Tangu niwaondoe watu wangu Israeli nchini Misri, sikuchagua mji wowote katika makabila ya Israeli ili nijengewe nyumba nitakamoabudiwa; ila nilimchagua Daudi, atawale watu wangu, Israeli.’ Kwa hiyo, baba yangu alikusudia kujenga nyumba atakamoabudiwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia baba yangu Daudi, ‘Ni vyema kwamba ulikusudia moyoni mwako kunijengea nyumba. Hata hivyo, si wewe utakayenijengea nyumba, ila mwanao utakayemzaa ndiye atakayenijengea hiyo nyumba.’ Na sasa, Mwenyezi-Mungu ametimiza ahadi yake, kwani nimekuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, na kukikalia kiti cha enzi cha Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyoahidi; pia nimejenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Zaidi ya hayo, nimetenga mahali pa kuweka sanduku la agano ambalo ndani yake mna agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na babu zetu, wakati alipowatoa katika nchi ya Misri.” Kisha Solomoni alisimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, naye, akiwa mbele ya jumuiya yote ya Waisraeli, aliinua mikono yake juu, akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu mwingine kama wewe, juu mbinguni, ama chini duniani! Wewe u mwaminifu, kwani umetimiza agano lako na kuwaonesha fadhili zako watumishi wako wanaoishi wakikutii kwa moyo wao wote. Umetimiza ahadi uliyoitoa kwa mtumishi wako Daudi baba yangu; naam, yale uliyonena umeyatimiza leo kwa uwezo wako mwenyewe. Kwa hiyo, sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninakuomba pia utimize ile ahadi uliyomwahidi mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ukisema: ‘Siku zote utakuwa na mzawa wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, iwapo wazawa wako watakuwa waangalifu kuhusu mwenendo wao mbele yangu kama wewe ulivyofanya mbele yangu.’ Basi, ee Mungu wa Israeli, nakusihi utimize hayo yote uliyomwahidi mtumishi wako, Daudi baba yangu. “Lakini, ee Mungu, kweli utakaa duniani? Ikiwa hata mbingu zenyewe wala mbingu za juu sana hazikutoshi, itakutoshaje nyumba hii ambayo nimeijenga? Hata hivyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mimi mtumishi wako nakuomba unisikie na kunitimizia ombi langu ninaloomba leo. Ichunge nyumba hii usiku na mchana, mahali ambapo umesema, ‘Hapo ndipo watu watakapoliheshimu jina langu;’ unisikie ninapokuja mahali hapa kuomba. Sikia maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watu wako Israeli wanapoomba wakielekea mahali hapa. Usikie maombi kutoka huko mbinguni; na ukisha sikia, utusamehe. “Mtu akimkosea mwenzake, naye akaletwa apate kuapa mbele ya madhabahu yako katika nyumba hii, naye akiapa, tafadhali wewe usikie kutoka huko mbinguni, uchukue hatua na kuwahukumu watumishi wako. Aliye na hatia umwadhibu kadiri ya makosa yake, asiye na hatia umwachilie na kumpatia tuzo kadiri ya uadilifu wake. “Ikiwa watu wako Waisraeli, wameshindwa na adui zao kwa sababu ya dhambi walizotenda dhidi yako, nao wakitubu kwako na kulikiri jina lako, wakiomba msamaha wako kwa unyenyekevu katika nyumba hii, basi, uwasikie kutoka huko mbinguni, uwasamehe watu wako Israeli dhambi zao, halafu uwarudishe katika nchi uliyowapa babu zao. “Mvua isiponyesha kwa sababu wametenda dhambi dhidi yako, wakiomba wakielekea mahali hapa na kulikiri jina lako, pia wakiziacha dhambi zao unapowaonya, tafadhali, uwasikie kutoka huko mbinguni, na usamehe dhambi za watumishi wako, watu wako Israeli, huku ukiwafundisha kufuata njia nyofu; ukanyeshe mvua katika nchi yako hii ambayo uliwapa watu wako iwe mali yako. “Iwapo kuna njaa nchini, au tauni, ukame, ugonjwa wa mimea, nzige au viwavi; au ikiwa watu wako wamezingirwa na adui zao katika mji wao wowote ule; ikiwa kuna pigo lolote au ugonjwa wowote, tafadhali, usikie maombi yoyote yatakayoombwa na watu wako, Israeli, au yatakayoombwa na mtu yeyote au watu wako wote wa Israeli; kila mtu akijua taabu za moyoni mwake, akikuomba huku akinyosha mikono yake kuelekea kwenye nyumba hii. Basi, usikie huko kwako mbinguni, utoe msamaha na kuchukua hatua; pia umtendee kila mtu kadiri anavyostahili (kwani ni wewe tu ujuaye mawazo ya mioyo ya wanadamu wote); ili wakutii wakati wote wanapoishi katika nchi uliyowapa babu zetu. “Vivyo hivyo, wakati mgeni asiye mmoja wa watu wako Israeli akija kutoka nchi ya mbali kwa ajili ya jina lako (maana watu wa mataifa mengine watasikia sifa zako na kuhusu nguvu na uwezo wako), mtu huyo akija na kuomba katika nyumba hii, nakusihi umsikie kutoka huko mbinguni, na umjalie huyo mgeni yote atakayokuomba; kusudi watu wote ulimwenguni wapate kujua jina lako na kukutii kama wafanyavyo watu wako, Israeli, na wapate kufahamu kwamba nyumba hii ambayo nimeijenga, inajulikana kwa jina lako. “Watu wako wakienda vitani kupigana na adui yao kokote kule utakakowapeleka, nao wakikuomba wakielekea mji uliouchagua na nyumba niliyoijenga kwa ajili ya jina lako, nakusihi usikie sala yao na maombi yao huko mbinguni, uwapatie ushindi vitani. “Ikiwa watatenda dhambi dhidi yako maana hakuna mtu asiyetenda dhambi, nawe ukiwakasirikia na kuwaacha washindwe na adui, hata wapelekwe mateka mpaka nchi ya adui iliyoko mbali au karibu; kama watakapokuwa huko uhamishoni watajirudi moyoni na kutubu na kukuomba msamaha, wakisema, ‘Tumetenda dhambi; tumepotoka na kufanya maovu;’ pia wakati huo watakapokuwa katika nchi ya adui zao, wakitubu kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote, na kama watakuomba wakielekea nchi yao ambayo uliwapatia babu zao, wakielekea mji huu ambao uliuchagua na nyumba hii ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako, basi, nakusihi kutoka huko mbinguni uliko usikie sala yao na ombi lao uwapatie haki zao. Uwasamehe watu wako dhambi walizotenda dhidi yako na uasi wao, uwahurumie mbele ya adui zao, ili nao wapate kuwahurumia, maana ni watu wako, na ni mali yako; watu ambao uliwatoa Misri kutoka katika tanuri ya chuma. “Uangalie ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako, Israeli, uwasikie kila wanapokuomba. Kwa sababu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu uliwatenga na watu wa mataifa mengine duniani, ili wawe mali yako — kama ulivyotangaza kwa njia ya Mose, mtumishi wako, wakati ule ulipowatoa babu zetu katika nchi ya Misri.” Solomoni alipomaliza kusema sala hiyo yote na ombi lake kwa Mwenyezi-Mungu aliinuka kutoka pale mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, mahali alipokuwa amepiga magoti akiinua mikono yake juu. Alisimama, akawabariki Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika hapo, akisema kwa sauti kubwa, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewapatia starehe watu wake Israeli, kulingana na ahadi yake. Ametimiza ahadi zake zote njema alizozitoa kupitia kwa mtumishi wake Mose. Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, awe nasi, kama alivyokuwa na babu zetu; tunaomba asituache, wala asitutupe. Yeye aelekeze mioyo yetu kwake, ili tufuate njia zake, tukishika amri zake, maongozi yake na maagizo yake aliyowapa babu zetu. Basi, maneno yangu haya ambayo ni ombi langu mbele ya Mwenyezi-Mungu, yawe karibu na Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mchana na usiku, naye amjalie mtumishi wake, na watu wake Israeli, ili wafanikiwe katika haja zao za kila siku. Nayo mataifa yote ulimwenguni yatajua kwamba kweli Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu; wala hakuna mwingine. Nanyi, muwe waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mkifuata masharti yake na kutii amri zake zote kama mnavyofanya hivi leo.” Kisha, mfalme Solomoni na Waisraeli wote waliokuwa pamoja naye walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko. Naye Solomoni alimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za amani: Ng'ombe 22,000 na kondoo 120,000. Hivyo ndivyo mfalme na watu wote wa Israeli walivyoiweka wakfu nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Siku hiyohiyo, mfalme aliiweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwani hapo ndipo alipotolea sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba haikutosha sadaka hizo zote. Naye Solomoni kwa muda wa siku saba na siku saba zaidi, yaani kwa siku kumi na nne, alifanya sikukuu pamoja na Waisraeli wote; nao walitoka tangu kiingilio cha Hamathi, hadi mto wa Misri. Katika siku ya nane, Solomoni aliwaaga watu; nao wakamtakia baraka mfalme, wakaenda kwao wakishangilia na kufurahi kwa sababu ya wema ambao Mwenyezi-Mungu aliuonesha kwa Daudi, mtumishi wake, na kwa watu wake Israeli Mfalme Solomoni alipomaliza kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu na majengo mengine yote aliyokusudia kujenga, Mwenyezi-Mungu alimtokea tena kama alivyomtokea kule Gibeoni. Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Nimesikia sala yako na ombi lako. Nimeitakasa nyumba hii ambayo umenijengea ili watu waliabudu jina langu hapa milele. Nitaichunga na kuipenda wakati wote. Nawe kama ukinitumikia kwa unyofu wa moyo na uadilifu kama baba yako Daudi alivyofanya, ukitii amri zangu na kutimiza yale yote niliyokuamuru, ukifuata masharti yangu na maagizo yangu; basi, mimi nitakiimarisha kiti chako cha kifalme juu ya Israeli milele, kama nilivyomwahidi Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa mtu wa kukaa juu ya kiti cha enzi cha Israeli. Lakini wewe au watoto wako mkigeuka na kuacha kunifuata, msiposhika amri zangu na maongozi niliyowapani, mkienda kutumikia miungu mingine na kuiabudu, basi, nitawahamisha watu wangu, Israeli, kutoka nchi hii ambayo nimewapa; kadhalika na nyumba hii ambayo nimeiweka wakfu kwa ajili ya jina langu, nitaitupilia mbali nami, na kuifanya kitu cha kupuuzwa na kudharauliwa miongoni mwa mataifa yote. Na nyumba hii itabomoka na kuwa magofu; kila apitaye karibu atashtuka na kutikisa kichwa, na kuuliza, ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu amefanya hivyo kwa nchi hii na kwa nyumba hii?’ Watu wengine watajibu, ‘Ni kwa sababu walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, aliyewatoa babu zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia; kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu amewaletea maafa haya yote.’” Kisha miaka ishirini ilipokwisha pita, ambayo Solomoni alizijenga zile nyumba mbili: Nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu, mfalme Solomoni alimpa Hiramu mfalme wa Tiro, miji ishirini katika mkoa wa Galilaya (kwa sababu huyo Hiramu alikuwa amempelekea Solomoni mbao za mierezi na miberoshi, na dhahabu pia, kadiri alivyohitaji kwa ujenzi). Lakini Hiramu alipowasili kutoka Tiro na kuiona miji hiyo aliyokuwa amepewa na Solomoni hakupendezwa nayo. Basi, akamwuliza Solomoni, “Ndugu yangu, ni miji gani hii ambayo umenipa?” Ndio sababu miji hiyo inaitwa nchi ya Kabuli hata leo. Hiramu alikuwa amempelekea mfalme Solomoni dhahabu kilo 3,600. Yafuatayo ni maelezo juu ya jinsi mfalme Solomoni alivyotumia kazi za kulazimishwa kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu yake, ngome ya Milo na ukuta wa Yerusalemu, na pia katika kujenga upya miji ya Hazori, Megido na Gezeri; (Gezeri ndio mji ambao Farao, mfalme wa Misri, alikuwa ameuteka, akauchoma moto na kuwaua Wakanaani, wakazi wake. Baadaye, binti Farao alipoolewa na Solomoni, mfalme wa Misri alimpa binti yake mji huo wa Gezeri uwe zawadi ya harusi. Basi, Solomoni aliujenga upya mji wa Gezeri); hali kadhalika alijenga Beth-horoni ya chini; kadhalika miji ifuatayo: Baalathi, na Tamari, mji ulio nyikani katika nchi ya Yuda na miji yake yote ya ghala, magari yake ya kukokotwa, na wapandafarasi wake; pia chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, Lebanoni au kwingineko katika ufalme wake. Watu wengine wote waliobaki miongoni mwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, yaani wote hao ambao hawakuwa wa taifa la Israeli, pamoja na wazawa wao ambao Waisraeli hawakuweza kuwaangamiza kabisa, Solomoni aliwafanyiza kazi za kulazimishwa hata leo. Lakini kati ya Waisraeli, Solomoni hakumfanya mtu yeyote kuwa mtumwa; wao ndio waliokuwa askari, watumishi wake, makamanda wake, maofisa wake, makamanda wa magari yake ya kukokotwa, na wapandafarasi wake. Ifuatayo ndiyo jumla ya maofisa wakuu waliohusika na uangalizi wa kazi ya Solomoni: Watu 550, hao ndio waliosimamia watu waliofanya kazi. Baadaye binti Farao aliuhama mji wa Daudi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe ambayo Solomoni alimjengea; kisha Solomoni akajenga ngome ya Milo. Mara tatu kila mwaka, Solomoni alitoa tambiko za kuteketezwa na tambiko za amani juu ya madhabahu aliyokuwa amemjengea Mwenyezi-Mungu, akamfukizia Mwenyezi-Mungu ubani; pia alifanya marekebisho ya nyumba. Mfalme Solomoni aliunda merikebu nyingi huko Esion-geberi, karibu na Elothi iliyo pwani ya Bahari ya Shamu, katika nchi ya Edomu. Naye mfalme Hiramu akawatuma maofisa wake na mabaharia pamoja na watumishi wa Solomoni. Walisafiri kwenda nchi ya Ofiri, na kuchukua toka huko dhahabu, wakamletea mfalme Solomoni kadiri ya kilo 14,000. Malkia wa Sheba aliposikia sifa za Solomoni, kwa sababu ya jina la Mwenyezi-Mungu, alimwendea Solomoni ili kumjaribu kwa maswali magumu. Aliwasili akiwa amefuatana na msafara wa watu pamoja na ngamia waliobeba manukato, zawadi nyingi sana na vito vya thamani. Naye Solomoni akayajibu maswali yote; hapakuwa na swali lolote lililomshinda. Malkia wa Sheba alishangaa sana alipoiona hekima yote ya Solomoni, na nyumba aliyokuwa ameijenga; tena alipoona chakula kilicholetwa mezani mwake, jinsi maofisa walivyoketi mezani, jinsi watumishi walivyohudumu na walivyovalia, pia wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa ambazo alizitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, aliduwaa na kushangaa mno. Basi, akamwambia mfalme, “Mambo yote niliyosikia nchini kwangu kuhusu kazi zako na hekima yako ni kweli! Lakini sikuweza kuamini habari hizo mpaka nilipofika na kujionea mwenyewe. Kumbe sikuambiwa hata nusu yake; hekima yako na fanaka zako vimepita habari nilizopewa. Wana bahati wake zako! Wana bahati hawa watumishi wako ambao wanakuhudumia daima na kusikiliza hekima yako! Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ambaye amependezwa nawe, akakuweka juu ya kiti cha enzi cha Israeli! Kwa sababu Mwenyezi-Mungu alipenda Israeli milele, amekuweka wewe uwe mfalme, ili udumishe haki na uadilifu.” Kisha malkia akampa mfalme zaidi ya kilo 4,000 za dhahabu, kiasi kikubwa cha manukato na vito vya thamani. Manukato kiasi kikubwa kama hicho alichomtolea mfalme Solomoni hakijapata kamwe kuletwa tena. Tena, msafara wa meli za Hiramu ulioleta dhahabu kutoka Ofiri, ulileta kwa wingi miti ya msandali na vito vya thamani. Naye mfalme aliitumia miti hiyo ya msandali kwa ajili ya nguzo za nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na za ikulu na pia kwa kutengenezea vinubi na vinanda vya waimbaji. Kiasi cha miti ya msandali kama hicho hakijaonekana tena mpaka leo. Mfalme Solomoni naye alimpatia malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na alichotaka; pamoja na vitu vingine ambavyo Solomoni alimpa kutokana na ukarimu wake wa kifalme. Basi malkia akarudi nchini kwake pamoja na watumishi wake. Kila mwaka, Solomoni alipelekewa dhahabu kilo 22,000. Kiasi hicho si pamoja na dhahabu aliyopata kwa wafanyabiashara na wachuuzi, kwa wafalme wote wa Arabia na wakuu wa mikoa ya Israeli. Mfalme Solomoni alitengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao kilo 7 za dhahabu. Alitengeneza ngao ndogondogo 300 kwa dhahabu iliyofuliwa, kila ngao kilo 1.5; halafu mfalme akaziweka katika jengo lililoitwa Nyumba ya Msitu wa Lebanoni. Vilevile mfalme alitengeneza kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakipaka dhahabu safi kabisa. Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita. Sehemu ya juu ilikuwa imeviringwa na kiliwekewa mahali pa kuegemeza mkono pande zake mbili; na sanamu za simba wawili zimesimama moja kando ya mahali hapo pa kuegemeza mkono. Kulikuwa pia na sanamu kumi na mbili za simba zimesimama, moja mwishoni mwa kila ngazi. Kiti kama hicho hakijawahi kutengenezwa katika ufalme wowote ule. Vyombo vyote vya kunywea divai vya mfalme Solomoni vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vilivyokuwa katika Nyumba ya Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi; hakuna kilichotengenezwa kwa madini ya fedha kwani madini ya fedha haikuthaminiwa kuwa kitu wakati huo. Kwa kuwa mfalme Solomoni alikuwa na msafara wa meli za Tarshishi zilizokuwa zikisafiri pamoja na meli za Hiramu, kila mwaka wa tatu meli hizo za Tarshishi zilimletea mfalme dhahabu, fedha, pembe, nyani na tausi. Hivyo, mfalme Solomoni aliwapita wafalme wote duniani kwa mali na hekima. Watu wa nchi zote walikuwa na hamu ya kumwendea Solomoni ili kusikiliza hekima yake ambayo Mungu alikuwa amemjalia. Kila mmoja wao alimletea zawadi: Vyombo vya fedha, vya dhahabu, mavazi, manemane, manukato, farasi na nyumbu. Zawadi hizi alizipokea kila mwaka. Solomoni alikusanya magari ya farasi na wapandafarasi, alikuwa na magari ya farasi 1,400 na wapandafarasi 12,000 ambao aliwaweka katika miji yenye vituo vya magari ya farasi, na huko Yerusalemu. Basi, Solomoni alifanya madini ya fedha katika Yerusalemu kuwa kitu cha kawaida kama mawe, na mbao za mierezi zilikuwa nyingi kama mbao za mikuyu ya Shefela. Solomoni aliagiza farasi kutoka Misri, na pia kutoka Kilikia ambako wafanyabiashara wake waliuziwa na watu wa Kilikia. Gari moja la kukokotwa liliweza kununuliwa huko Misri kwa fedha ipatayo kilo 7, na farasi mmoja aliweza kugharimu fedha kilo 2. Wafanyabiashara wa mfalme walisafirisha magari na farasi hao na kuwauzia wafalme wote wa Wahiti na wa Wasiria. Solomoni alipenda sana wanawake wa kigeni: Binti Farao, wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni, na Wahiti; wanawake wa mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amewakataza Waisraeli akisema, “Msioe kwao wala wao wasioe kwenu kwa sababu wanawake hao watapotosha mioyo yenu ili muitumikie miungu yao.” Solomoni aliwapenda sana wanawake hao. Solomoni akawa na wanawake 700, wote mabinti wa kifalme; na masuria 300. Hao wanawake wakampotosha. Maana, alipokuwa mzee, wake zake walimpotosha hata akaitumikia miungu mingine, wala hakuwa mwaminifu kabisa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama baba yake Daudi alivyokuwa mwaminifu. Solomoni alimtumikia Ashtarothi aliyekuwa mungu wa kike wa Wasidoni, na alimfuata Milkomu chukizo la Waamoni. Hivyo, Solomoni alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wala hakufuata kwa ukamilifu matakwa ya Mwenyezi-Mungu kama baba yake Daudi alivyokuwa amefanya. Juu ya mlima ulio mashariki ya Yerusalemu, Solomoni alijenga mahali pa kumtambikia Kemoshi, chukizo la Wamoabu, na mahali pa kumtambikia Moleki, chukizo la Waamoni. Kadhalika, aliwajengea wake zake wote wa kigeni mahali pa kufukizia ubani na kuitambikia miungu yao. Basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alimkasirikia Solomoni, kwa sababu alikuwa amemwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ingawa yeye alikuwa amemtokea mara mbili, na kumwamuru asiiabudu miungu ya kigeni; Solomoni hakutii amri ya Mwenyezi-Mungu. Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa umeamua kufanya hivyo, ukavunja agano langu nawe, na kuasi amri zangu nilizokupa, hakika nitakunyanganya huo utawala na kumpa mtumishi wako. Hata hivyo, kwa ajili ya baba yako Daudi, sitafanya hivyo maishani mwako, bali nitauondoa utawala huo mikononi mwa mwanao. Hata yeye sitamnyanganya milki yote, bali nitamwachia mwanao kabila moja, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya mji wa Yerusalemu ambao nimeuchagua kuwa wangu.” Ndipo Mwenyezi-Mungu akamfanya Hadadi aliyekuwa wa ukoo wa mfalme wa Edomu, kuwa adui ya Solomoni. Wakati Daudi alipowaangamiza Waedomu Yoabu, mkuu wa jeshi la Daudi, alikwenda huko kuwazika waliouawa. Yoabu aliwaua wanaume wote wa Edomu. (Yoabu alikaa huko na wanajeshi wake kwa muda wa miezi sita, apate kuwaangamiza kabisa wanaume wote wa Edomu.) Lakini Hadadi ambaye wakati huo alikuwa kijana alitorokea Misri pamoja na Waedomu kadhaa, watumishi wa baba yake. Hadadi na wenzake walisafiri kutoka Midiani, wakawachukua watu wengine huko Parani, wakaenda nao mpaka Misri, kwa Farao mfalme wa nchi hiyo. Farao akampatia Hadadi nyumba, akaamuru awe akipewa chakula, akampa na ardhi. Farao alipendezwa sana na Hadadi. Hivyo Farao akamruhusu shemeji yake, mdogo wa malkia Tapenesi, aolewe na Hadadi. Huyo dada wa Tapenesi akamzalia Hadadi mwana aliyeitwa Genubathi. Genubathi alilelewa na Tapenesi katika nyumba ya Farao, pamoja na wana wa mfalme. Lakini Hadadi aliposikia huko Misri kwamba Daudi na Yoabu mkuu wa jeshi, walikuwa wamefariki, alimwambia Farao, “Uniruhusu niondoke nirudi nchini kwangu.” Lakini Farao akamwuliza, “Nimekunyima nini hata uamue sasa kurudi nchini kwako?” Naye Hadadi akamsihi akisema, “Uniache tu niende.” Vilevile, Mungu alimfanya Rezoni mwana wa Eliada, awe adui ya Solomoni. Rezoni alikuwa amemtoroka bwana wake, mfalme Hadadezeri wa Soba. Baada ya Daudi kufanya mauaji huko Soba, Rezoni alikusanya watu na kuunda genge la maharamia, naye mwenyewe akawa kiongozi wao. Basi, wakaenda Damasko, wakakaa huko na kumfanya Rezoni mfalme wa Damasko. Rezoni alikuwa adui wa Israeli siku zote za utawala wa Solomoni, akamsumbua sana Solomoni kama naye Hadadi alivyomsumbua. Basi, Rezoni aliidharau Israeli, naye alitawala nchi ya Aramu. Yeroboamu mwana wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumishi wa Solomoni, ambaye mama yake mjane, aliitwa Zerua, pia alimwasi mfalme. Kisa cha uasi huo ni hiki: Solomoni alipokuwa akishughulika na kusawazisha sehemu ya Milo, na kuimarisha kuta za mji wa baba yake Daudi, Yeroboamu alionekana kuwa kijana hodari na shujaa. Ndipo Solomoni alipoona kwamba huyo kijana alikuwa mwenye bidii, akamweka awe msimamizi wa kazi za kulazimishwa zilizofanywa na watu wa ukoo wa Yosefu. Siku moja, Yeroboamu alipokuwa akisafiri kutoka Yerusalemu, nabii Ahiya wa Shilo alikutana naye njiani. Ahiya alikuwa amevaa vazi jipya. Wote wawili walikuwa peke yao mashambani. Mara, Ahiya akalivua vazi lake jipya, akalirarua vipande kumi na viwili, halafu akamwambia Yeroboamu, “Jitwalie vipande kumi maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Tazama, karibu nitaurarua ufalme na kuuondoa mikononi mwa Solomoni, nami nitakupa wewe makabila kumi.’ Lakini yeye nitamwachia kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya mji wa Yerusalemu ambao nimeuchagua kuwa wangu katika makabila yote ya Israeli. Nitafanya hivyo kwa sababu Solomoni ameniacha, akaabudu miungu ya kigeni: Ashtarothi mungu wa kike wa Wasidoni, Kemoshi, mungu wa Wamoabu na Milkomu mungu wa Waamoni. Solomoni ameniasi, ametenda maovu mbele yangu, na wala hakutii sheria zangu na maagizo yangu kama Daudi baba yake alivyofanya. Hata hivyo, sitamnyanganya milki yote, wala sitamwondolea mamlaka maishani mwake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi ambaye nilimchagua, na ambaye alifuata amri zangu na maongozi yangu. Lakini, nitamnyanganya mwanawe ufalme huo, nami nitakupatia wewe Yeroboamu makabila kumi. Huyo mwanawe Solomoni nitamwachia kabila moja, ili wakati wote mzawa wa mtumishi wangu Daudi awe anatawala Yerusalemu, awe taa inayoangaza daima mbele yangu katika mji ambao nimeuchagua uwe mahali pa kuniabudia. Basi, wewe Yeroboamu, nitakufanya kuwa mfalme wa Israeli, nawe utatawala kama upendavyo. Na kama utazingatia yote nitakayokuamuru, kama utaishi kulingana na matakwa yangu, kama utatenda mema mbele zangu kwa kushika maongozi yangu na amri zangu, kama mtumishi wangu Daudi alivyofanya, mimi nitakuwa pamoja nawe daima. Na nitakupatia nchi ya Israeli na kuufanya utawala wako uwe thabiti kama nilivyomfanyia Daudi. Kutokana na hayo, nitawaadhibu wazawa wa Daudi, lakini si daima.” Kwa sababu hiyo, Solomoni alijaribu kumuua Yeroboamu; lakini Yeroboamu akakimbilia Misri kwa Shishaki mfalme wa Misri, akakaa huko mpaka Solomoni alipofariki. Mambo mengine ya Solomoni, yote aliyotenda na hekima yake, yameandikwa katika Kitabu cha Matendo ya Solomoni. Kwa muda wa miaka arubaini, Solomoni aliitawala nchi yote ya Israeli; makao yake yakiwa Yerusalemu. Hatimaye, Solomoni alifariki, akazikwa katika mji wa baba yake Daudi. Rehoboamu, mwanawe Solomoni, akatawala mahali pake. Basi, Rehoboamu akaenda Shekemu ambako Waisraeli wote walikuwa wamekusanyika ili kumtawaza awe mfalme. Naye Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari kuhusu tendo hilo (maana alikuwa bado Misri ambako alikwenda alipomkimbia Solomoni), alirudi kutoka Misri. Lakini Waisraeli walituma ujumbe na kumwita. Kisha, yeye pamoja na jumuiya yote ya Israeli, walimwendea Rehoboamu, wakamwambia, “Baba yako alitutwisha mzigo mzito. Basi, utupunguzie mzigo huo, nasi tutakutumikia.” Naye Rehoboamu akawaambia, “Nendeni, mrudi kwangu kesho kutwa.” Basi, wakaondoka. Baadaye Rehoboamu alitaka kujua maoni ya wazee ambao walikuwa washauri wa baba yake Solomoni, alipokuwa angali hai, akawauliza, “Je, mnanishauri niwape jibu gani watu hawa?” Wazee hao wakamjibu, “Leo ukiwa mtumishi wa watu hawa, ukawatumikia na kuongea nao vizuri unapowajibu, hapo watakuwa watumishi wako daima.” Lakini Rehoboamu alipuuza shauri la wazee; badala yake akashauriana na vijana wa rika lake ambao walikuwa washauri wake. Basi, akawauliza, “Nyinyi mnatoa shauri gani ili tuweze kuwajibu watu hawa walioniambia niwapunguzie mzigo ambao baba yangu aliwatwika?” Hao vijana wakamjibu, “Watu hao waliokuambia baba yako aliwatwika mzigo mzito, wakakuomba uwapunguzie mzigo huo, wewe waambie hivi: ‘Kidole changu kidogo ni kinene zaidi kuliko kiuno cha baba yangu. Mzigo wa baba yangu ulikuwa mzito, lakini wangu utakuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.’” Basi, siku ya tatu Yeroboamu pamoja na watu wote wakarudi kwa Rehoboamu kama alivyokuwa amewaagiza. Mfalme akawajibu watu hao kwa ukali, akapuuza shauri alilopewa na wazee, akafuata shauri la vijana wenzake, akawaambia, “Baba yangu aliwatwika mzigo mzito, lakini mimi nitaufanya kuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.” Hivyo, mfalme hakuwajali watu kwa sababu jambo hili lilisababishwa na Mwenyezi-Mungu, ili atimize neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati, kwa njia ya Ahiya wa Shilo. Lakini watu wote wa Israeli walipoona kwamba mfalme hakuwajali, walimwambia, “Hatuna uhusiano wowote na Daudi! Hatuna sehemu yetu kutoka kwa huyo mwana wa Yese. Rudini nyumbani, enyi watu wa Israeli! Itunze nyumba yako mwenyewe, ee Daudi.” Hivyo, watu wa Israeli wakarudi makwao. Watu wa Israeli waliokuwa wanakaa katika miji ya Yuda, ndio hao tu waliobaki chini ya utawala wa Rehoboamu. Mfalme Rehoboamu alipomtuma Adoramu, aliyekuwa mnyapara mkuu wa kazi za kulazimishwa, watu wote wa Israeli walimpiga mawe, wakamuua. Naye Rehoboamu alipanda haraka gari lake la kukokotwa, akakimbilia Yerusalemu. Hivyo watu wa Israeli wamekuwa katika hali ya uasi dhidi ya ukoo wa Daudi mpaka leo. Watu wote wa Israeli walipopata habari kwamba Yeroboamu alikuwa amerudi kutoka Misri, walimwita katika mkutano wa hadhara, wakamtawaza kuwa mfalme wa Israeli yote. Hakuna kabila lingine lililojiunga na ukoo wa Daudi isipokuwa tu kabila la Yuda. Rehoboamu alipofika Yerusalemu, alikusanya askari stadi 180,000 wa makabila ya Yuda na Benyamini, apate kupigana na utawala wa Israeli, ili aurudishe utawala kwake yeye mwenyewe Rehoboamu, mwana wa Solomoni. Lakini ujumbe wa Mungu ulimjia Shemaya, mtu wa Mungu: “Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni, mfalme wa Yuda, na watu wote wa kabila la Yuda na Benyamini na watu wengine, kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: ‘Msiende, wala msipigane na ndugu zenu, watu wa Israeli. Rudini kila mtu nyumbani kwake, maana hayo yaliyotokea ni mpango wangu.’” Basi, wakaufuata ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu, wakarudi nyumbani tena, kama Mwenyezi-Mungu alivyoagiza. Baadaye mfalme Yeroboamu akaujenga upya mji wa Shekemu kwenye mlima wa Efraimu; akakaa huko. Kisha akaenda akajenga mji wa Penueli. Ndipo Yeroboamu akaanza kufikirifikiri: “Sasa ufalme utarudi kwa jamaa ya mfalme Daudi kama watu hawa wataendelea kwenda kutambikia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu. Mioyo yao itamgeukia bwana wao Rehoboamu mfalme wa Yuda, nao wataniua mimi.” Basi, baada ya kushauriana na wengine, akatengeneza sanamu za ndama mbili za dhahabu. Kisha akawaambia watu, “Enyi watu wa Israeli, hii ndiyo miungu yenu iliyowatoa katika nchi ya Misri! Hakuna sababu ya kwenda Yerusalemu kutambikia huko.” Akaweka sanamu moja ya ndama wa dhahabu mjini Betheli, na ya pili mjini Dani. Tendo hili likawa dhambi, maana watu waliandamana kwenda kuzitambikia sanamu hizo huko Betheli na Dani. Vilevile, Yeroboamu alijenga mahali pa kutambikia vilimani, akateua makuhani, watu ambao hawakuwa wa ukoo wa Lawi. Yeroboamu pia aliamuru siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane iwe sikukuu sawa na ile sikukuu iliyokuwa inafanyika huko Yuda. Alitoa tambiko kwenye madhabahu aliyotengeneza huko Betheli mbele ya zile sanamu za ndama alizozitengeneza, akaweka wale makuhani aliowateua wahudumu kila mahali pa kutolea tambiko alikotengeneza vilimani. Siku hiyo ya kumi na tano ya mwezi wa nane, aliibuni yeye mwenyewe, naye akaenda Betheli kutambikia. Ndivyo alivyoiimarisha sikukuu hiyo aliyoiweka kwa ajili ya watu wa Israeli, naye mwenyewe akapanda kuiendea madhabahu, kufukiza ubani. Siku moja Yeroboamu alikuwa amesimama kando ya madhabahu ili afukize ubani. Basi, mtu wa Mungu kutoka Yuda akawasili hapo Betheli na ujumbe wa Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo akailaani ile madhabahu akisema, “Ee madhabahu! Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Atazaliwa mtoto katika ukoo wa Daudi, jina lake Yosia. Huyo atawatwaa makuhani wanaohudumu mahali pa ibada na kufukiza ubani juu yako, na kutambika juu yako; naam, mifupa ya watu itateketezwa juu yako!’” Mtu huyo akatoa ishara siku ileile, akasema: “Hii ndiyo ishara aliyotamka Mwenyezi-Mungu: ‘Madhabahu itabomoka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.’” Mfalme Yeroboamu aliposikia maneno hayo ya mtu wa Mungu dhidi ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono akasema, “Mkamateni huyo!” Na mara huo mkono wake aliounyosha, ukakauka, asiweze tena kuukunja. Madhabahu nayo ikabomoka, na majivu yake yakamwagika chini, kama ishara ile aliyoitoa huyo mtu wa Mungu na ujumbe wa Mwenyezi-Mungu. Basi, mfalme Yeroboamu akamwambia nabii, “Tafadhali, umsihi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, uniombee mkono wangu upate kupona.” Naye nabii akamwomba Mwenyezi-Mungu, na mkono wa mfalme ukapona, ukarudia hali yake ya hapo awali. Ndipo mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Karibu nyumbani kwangu kula chakula, nami nikupe zawadi.” Lakini mtu wa Mungu akamwambia, “Hata kama ukinipa nusu ya milki yako, sitakwenda pamoja nawe. Sitakula wala kunywa maji mahali hapa, kwani Mwenyezi-Mungu aliniamuru nisile chakula au kunywa maji, wala nisirudi kwa njia ileile niliyoifuata kuja hapa.” Basi, mtu huyo akaenda zake, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli. Wakati huo, palikuwa na nabii mmoja mzee huko Betheli. Wanawe wakamwendea, wakamweleza mambo yote aliyotenda yule mtu wa Mungu siku hiyo, huko Betheli; wakamwambia pia yale maneno yule mtu aliyomwambia mfalme Yeroboamu. Baba yao akawauliza, “Amefuata njia ipi?” Nao wakamwonesha njia aliyoifuata huyo mtu wa Mungu kutoka Yuda. Naye akawaambia watoto wake, “Nitandikieni huyo punda.” Nao wakamtandikia punda, na mzee akapanda juu yake. Akamfuata yule mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mti wa mwaloni. Basi, akamwuliza, “Je, wewe ndiwe yule mtu wa Mungu kutoka Yuda?” Naye akamjibu, “Naam! Mimi ndiye.” Huyo mzee akamwambia, “Karibu nyumbani kwangu, ukale chakula.” Lakini yeye akamwambia, “Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia nyumbani kwako. Siwezi kula chakula au kunywa maji mahali hapa, maana, Mwenyezi-Mungu aliniamuru nisile chakula au kunywa maji mahali hapa, wala nisirudi kwa njia niliyoijia.” Huyo mzee wa Betheli akamwambia, “Mimi pia ni nabii kama wewe, na Mwenyezi-Mungu amenena nami kwa njia ya malaika akisema, ‘Mrudishe nyumbani kwako, ale chakula na kunywa maji.’” Lakini huyo nabii mzee alikuwa anamdanganya tu. Basi, mtu wa Mungu akarudi pamoja naye, akala chakula na kunywa maji kwa huyo mzee. Walipokuwa mezani, neno la Mwenyezi-Mungu likamjia huyo nabii mzee, naye akamwambia kwa sauti huyo mtu wa Mungu kutoka Yuda: “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Wewe umeacha kutii ujumbe wa Mwenyezi-Mungu; wewe hukufuata amri aliyokupa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Badala yake, umerudi hapa, ukala chakula na kunywa maji mahali hapa ambapo uliambiwa usile chakula wala kunywa maji. Basi, mwili wako hautazikwa kwenye kaburi la babu zako.’” Walipomaliza kula, huyo nabii mzee akamtandikia punda huyo mtu wa Mungu, naye akaondoka. Alipokuwa anakwenda zake, simba akakutana naye njiani, akamuua; mwili wake ukawa umetupwa hapo barabarani; punda wake na huyo simba wakawa wamesimama kando yake. Watu waliopitia hapo na kuiona maiti barabarani, na simba amesimama karibu nayo, wakaenda mpaka mjini alimokuwa anakaa yule nabii, wakawaambia watu. Nabii yule ambaye alikuwa amemkaribisha nyumbani kwake aliposikia habari hiyo, akasema, “Huyo ni yuleyule mtu wa Mungu aliyekataa kutii neno la Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu amemtuma simba, akamshambulia na kumwua kama alivyokuwa amemwambia.” Hapo akawaambia wanawe “Nitandikie punda.” Nao wakamtandikia. Mzee akaenda, akaikuta maiti ya mtu wa Mungu barabarani, simba na punda wake kando yake; huyo simba hakuila maiti wala hakumshambulia punda. Basi, huyo nabii mzee akaitwaa maiti ya mtu wa Mungu, akaiweka juu ya punda wake, akairudisha mjini Betheli, kuomboleza kifo chake na kumzika. Basi, akamzika katika kaburi lake, naye pamoja na wanawe wakaomboleza kifo chake wakisema, “Aa! Ndugu yangu!” Baada ya mazishi, nabii huyo akawaambia wanawe, “Nikifa, nizikeni katika kaburi hilihili alimozikwa mtu wa Mungu; mifupa yangu kando ya mifupa yake. Mambo yote aliyoagizwa na Mwenyezi-Mungu dhidi ya madhabahu ya Betheli, na mahali pote pa kutambikia vilimani Samaria, hakika yatatimia.” Yeroboamu hakuuacha upotovu wake; aliendelea kuteua watu wa kawaida kuwa makuhani, wahudumie mahali pa kutambikia vilimani. Mtu yeyote aliyejitolea, alimweka wakfu kuwa kuhani wa mahali pa kutambikia huko vilimani. Tendo hili likawa dhambi ambayo ilisababisha ukoo wa Yeroboamu ufutiliwe mbali na kuangamizwa. Wakati huo, Abiya mwana wa mfalme Yeroboamu, akawa mgonjwa. Yeroboamu akamwambia mkewe, “Jisingizie kuwa mwingine, uende mjini Shilo anakokaa nabii Ahiya aliyesema kwamba mimi nitakuwa mfalme wa Israeli. Mpelekee mikate kumi, maandazi kadha, na asali chupa moja. Yeye atakuambia yatakayompata mtoto wetu.” Basi, mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda Shilo nyumbani kwa Ahiya. Wakati huo, Ahiya alikuwa hawezi tena kuona sawasawa kwa sababu ya uzee. Mwenyezi-Mungu alikuwa amekwisha mwambia Ahiya kwamba mke wa Yeroboamu alikuwa njiani, anakuja kumwuliza yatakayompata mwanawe mgonjwa, na jinsi atakavyomjibu. Mkewe Yeroboamu alipofika, alijisingizia kuwa mtu mwingine. Lakini Ahiya alipomsikia anaingia mlangoni, alisema, “Karibu ndani mke wa Yeroboamu. Lakini mbona unajisingizia kuwa mtu mwingine? Ninao ujumbe usio mzuri kwako! Nenda ukamwambie Yeroboamu kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Nilikuteua miongoni mwa watu, nikakufanya kuwa kiongozi wa watu wangu, Israeli; nikaurarua ufalme utoke kwa wazawa wa Daudi, nikakupa wewe. Lakini wewe ni kinyume kabisa cha mtumishi wangu Daudi ambaye alizishika amri zangu, akafuata matakwa yangu kwa moyo wake wote na kutenda tu yaliyo sawa mbele ya macho yangu. Wewe umetenda uovu mbaya zaidi kuliko waliotenda wale waliokutangulia; wewe umenikasirisha kwa kujitengenezea miungu mingine na sanamu za kufua, kisha umeniacha. Haya basi, sasa nitailetea balaa jamaa hii yake, Yeroboamu, nitawaua wanaume wote wa jamaa zake katika Israeli, awe mtumwa au huru. Jamaa wake wote nitawateketeza kama mtu ateketezavyo mavi, mpaka yatoweke. Yeyote aliye wa jamaa ya Yeroboamu atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.’” Ahiya akamwambia mkewe Yeroboamu, “Haya inuka, uende zako nyumbani. Mara tu utakapoingia mjini, mwanao atakufa. Watu wote wa Israeli watafanya matanga na kumzika. Walakini, ni huyo tu wa jamaa ya Yeroboamu atakayezikwa, kwani ni yeye tu wa jamaa ya Yeroboamu aliyepata kumpendeza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Tena leo hii, Mwenyezi-Mungu ataweka mfalme mwingine katika Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Naam, tangu sasa, Mwenyezi-Mungu atawapiga watu wa Israeli, nao watatikisika kama unyasi unavyotikiswa mtoni. Atawangoa kutoka nchi hii nzuri aliyowapa babu zao, na kuwatawanya mbali, ngambo ya mto Eufrate, kwa sababu wamemkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa kujitengenezea sanamu za Ashera, mungu wa kike. Mwenyezi-Mungu ataitupa Israeli kwa sababu ya dhambi alizotenda Yeroboamu, na kuwafanya watu wa Israeli pia watende dhambi.” Hapo, mkewe Yeroboamu akaondoka, akashika safari mpaka Tirza. Mara tu alipofika mlangoni, mtoto akafa. Watu wote wa Israeli wakamzika na kufanya matanga kama alivyosema Mwenyezi-Mungu, kwa njia ya nabii Ahiya, mtumishi wake. Matendo mengine ya mfalme Yeroboamu, jinsi alivyopigana vita na alivyotawala, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Yeroboamu alitawala kwa muda wa miaka ishirini na miwili, halafu akafariki, na Nadabu, mwanawe, akatawala mahali pake. Rehoboamu, mwanawe Solomoni, alikuwa na umri wa miaka arubaini na mmoja alipoanza kutawala Yuda. Naye alitawala kwa muda wa miaka kumi na saba katika Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi-Mungu aliuchagua miongoni mwa miji ya makabila yote ya Israeli aabudiwe humo. Mama yake Rehoboamu alikuwa Naama kutoka Amoni. Watu wa Yuda walitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha kwa dhambi zao walizotenda, nyingi kuliko za babu zao. Walijitengenezea pia mahali pa ibada, minara ya kutambikia, na sanamu za Ashera, juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Tena, kukawa na ibada za ukahaba nchini; watu walitenda matendo ya kuchukiza ya mataifa ambayo Mungu aliyafukuza Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini Kanaani. Katika mwaka wa tano wa utawala wa Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri, aliushambulia mji wa Yerusalemu, akaichukua hazina yote ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya ikulu; alichukua kila kitu; pia alichukua ngao zote za dhahabu alizozitengeneza Solomoni. Badala ya ngao hizo, mfalme Rehoboamu alitengeneza ngao za shaba na kuziweka chini ya ulinzi wa wangojamlango wa ikulu. Kila wakati mfalme alipokwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walinzi walizibeba ngao hizo, na baadaye wakazirudisha katika chumba cha ulinzi. Matendo mengine ya mfalme Rehoboamu, na yote aliyoyafanya, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Daima kulikuwako vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. Hatimaye, Rehoboamu alifariki na kuzikwa kwenye makaburi ya wazee wake, katika mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama kutoka Amoni, na Abiyamu mwanawe akatawala mahali pake. Abiya alianza kutawala huko Yuda mnamo mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yeroboamu, mwanawe Nebati. Alitawala kwa muda wa miaka mitatu akiwa Yerusalemu. Mama yake alikuwa Maaka binti Absalomu. Abiya alitenda dhambi zilezile alizotenda baba yake, wala hakuwa na moyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama alivyokuwa babu yake Daudi. Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi, Mwenyezi-Mungu alimpatia Abiya mwana atakayetawala baada yake, kuwa taa ya kuangaza Yerusalemu na kuuweka imara mji wa Yerusalemu. Mwenyezi-Mungu alifanya hivyo kwa kuwa Daudi alitenda mema mbele yake na hakukiuka aliyomwamuru Mwenyezi-Mungu siku zake zote, isipokuwa tu ule mkasa wa Uria, Mhiti. Kulikuwako vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu wakati wote alipokuwa mtawala. Matendo mengine ya Abiya, na yote aliyoyafanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Abiya na Yeroboamu waliishi katika hali ya vita. Mwishowe, Abiya alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi na mwanawe Asa akatawala mahali pake. Mnamo mwaka wa ishirini wa utawala wa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, Asa alianza kutawala huko Yuda. Alitawala kwa muda wa miaka arubaini na mmoja. Mama yake alikuwa Maaka, binti Absalomu. Mfalme Asa alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyofanya Daudi babu yake. Aliwafukuza nchini wale wafiraji wa kidini, akaziondoa sanamu zote ambazo babu zake walikuwa wamezitengeneza. Alimvua Maaka, mama yake, cheo chake cha mama malkia, kwa sababu alitengeneza sanamu ya Ashera, mungu wa kike, na hiyo sanamu akaivunjavunja na kuiteketeza kwenye bonde la Kidroni. Lakini mahali pa juu pa kutambikia miungu hapakuharibiwa; hata hivyo, yeye alikuwa na moyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu maisha yake yote. Alirudisha nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu vyombo vyote vilivyokuwa vimewekwa wakfu na baba yake, pamoja na vile vyake yeye mwenyewe: Vyombo vya fedha, dhahabu na vyombo vinginevyo. Mfalme Asa wa Yuda, na mfalme Baasha wa Israeli, walikuwa na vita kati yao wakati wote walipokuwa wakitawala. Baasha, mfalme wa Israeli, aliishambulia nchi ya Yuda na kuanza kuujenga Rama ili apate kuzuia mtu yeyote asitoke wala asiingie kwa Asa, mfalme wa Yuda. Ndipo mfalme Asa akachukua fedha na dhahabu yote iliyobaki katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu, akawapa watumishi wake, akawatuma Damasko kwa Ben-hadadi mwana wa Tabrimoni, mjukuu wa Hezioni, mfalme wa Aramu, akasema, “Tufanye mkataba wa ushirikiano kati yangu na wewe kama vile walivyofanya baba yangu na baba yako; tazama, nimekupelekea zawadi ya fedha na dhahabu; nenda ukavunje mkataba wa ushirikiano ulioko kati yako na mfalme Baasha wa Israeli, ili aache mashambulizi dhidi yangu.” Hapo mfalme Ben-hadadi akakubali pendekezo la mfalme Asa, akawatuma majemadari wake na majeshi yake kwenda kuishambulia miji ya Israeli. Nao wakateka Iyoni, Dani, Abel-beth-maaka, Kinerethi yote, na nchi yote ya Naftali. Mfalme Baasha alipopata habari za mashambulizi hayo aliacha kuujenga mji wa Rama akaishi katika Tirza. Ndipo mfalme Asa alipotoa tangazo kwa watu wote wa Yuda, bila kumwacha hata mtu mmoja, wahamishe mawe ya Rama na mbao, vifaa ambavyo Baasha alivitumia kujengea. Kisha mfalme Asa alitumia vifaa hivyo kujengea Geba, katika Benyamini na Mizpa. Matendo mengine yote ya Asa, ushujaa wake na miji yote aliyoijenga, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Lakini, wakati wa uzee wake, Asa alishikwa na ugonjwa wa miguu. Hatimaye, Asa alifariki, akazikwa katika makaburi ya kifalme, katika mji wa Daudi, naye mwanawe Yehoshafati akatawala mahali pake. Mnamo mwaka wa pili wa utawala wa Asa huko Yuda, Nadabu, mwana wa Yeroboamu, alianza kutawala huko Israeli. Alitawala kwa muda wa miaka miwili. Nadabu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; akamwiga baba yake ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Baasha mwana wa Ahiya, wa kabila la Isakari, akala njama dhidi ya Nadabu. Basi, wakati Nadabu na jeshi lake walipokuwa wameuzingira mji wa Gibethoni wa Wafilisti, Baasha akamvamia na kumwua, akatawala mahali pake. Huo ulikuwa mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Asa wa Yuda. Mara tu alipoanza kutawala, Baasha akawaua watu wote wa jamaa ya Yeroboamu; hakuacha hai hata mtu mmoja wa jamaa ya Yeroboamu; hiyo ilikuwa sawa na yale aliyosema Mwenyezi-Mungu kwa njia ya mtumishi wake, Ahiya wa Shilo. Mambo haya yalifanyika kwa sababu Yeroboamu alimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa dhambi yake na kwa kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Matendo mengine ya Nadabu, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Mfalme Asa wa Yuda na mfalme Baasha wa Israeli walikuwa na vita kati yao wakati wote walipokuwa wakitawala. Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya, alianza kutawala Israeli kutoka Tirza. Alitawala kwa muda wa miaka ishirini na minne. Baasha alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamwiga Yeroboamu na kutenda dhambi ileile ambayo aliwafanya watu wa Israeli watende. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yehu mwana wa Hanani, dhidi ya Baasha: “Wewe Baasha, mimi nilikuinua kutoka mavumbini, nikakufanya kiongozi wa watu wangu Israeli. Wewe umemwiga Yeroboamu, ukawafanya watu wangu Israeli watende dhambi na kunikasirisha kwa dhambi zao. Haya! Sasa, nitakufutilia mbali wewe na jamaa yako; nitaitendea jamaa yako kama nilivyoitendea jamaa ya Yeroboamu mwana wa Nebati. Yeyote wa jamaa yako atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla.” Matendo mengine ya Baasha na ushujaa wake, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Hatimaye, Baasha alifariki, akazikwa huko Tirza; mwanawe Ela akatawala mahali pake. Tena neno la Mwenyezi-Mungu dhidi ya Baasha na jamaa yake, lilimjia Yehu mwanawe Hanani kwa sababu ya maovu aliyotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu. Baasha alimkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa matendo yake; alimwiga Yeroboamu na jamaa yake na kuiletea jamaa yake maangamizi. Mnamo mwaka wa ishirini na sita wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha, alianza kutawala huko Israeli kutoka Tirza. Alitawala kwa muda wa miaka miwili. Mtumishi wake Zimri ambaye alisimamia nusu ya kikosi cha magari yake ya kukokotwa, alikula njama juu yake. Siku moja, mfalme Ela alipokuwa huko Tirza nyumbani kwa Arsa aliyekuwa msimamizi wa ikulu, alikunywa, akalewa. Basi, Zimri akaingia ndani, akamuua. Kisha akatawala mahali pake. Huu ulikuwa mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Mara tu alipoanza kutawala, Zimri aliwaua watu wote wa jamaa ya Baasha; hakumwachia hata mwanamume mmoja wa jamaa yake wala wa rafiki zake; ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu dhidi ya Baasha, kwa njia ya nabii Yehu. Mambo haya yalifanyika kwa sababu ya dhambi alizotenda Baasha na mwanawe Ela. Walimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kutenda dhambi na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi kwa sanamu za miungu yao. Matendo mengine ya Ela, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Zimri alitawala huko Israeli kutoka Tirza kwa muda wa siku saba. Huo ulikuwa mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Basi, watu wa Israeli walikuwa wamepiga kambi kuuzingira mji wa Gibethoni wa Wafilisti, na majeshi ya watu wa Israeli waliposikia kwamba Zimri alikuwa amekula njama, akamuua mfalme, wote wakamtawaza Omri, amiri jeshi wao, kuwa mfalme wa Israeli siku hiyohiyo. Omri na majeshi yake akaondoka Gibethoni, akaenda na kuuzingira mji wa Tirza. Zimri alipoona kwamba mji umezingirwa, aliingia ngomeni, ndani ya ikulu, akaichoma moto, naye akafia humo. Jambo hilo lilifanyika kwa sababu ya dhambi alizotenda alifanya maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamwiga Yeroboamu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Matendo mengine ya Zimri na njama aliyokula, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Watu wa Israeli, sasa, waligawanyika makundi mawili: Kundi moja lilimtambua Tibni mwana wa Ginathi kuwa mfalme, na kundi la pili lilimtambua Omri. Hatimaye watu wa kundi lililomtambua Omri, wakawazidi nguvu wale waliomtambua Tibni mwanawe Ginathi; Tibni akafa na Omri akawa mfalme. Omri alianza kutawala mnamo mwaka wa thelathini na mmoja wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Alitawala kwa muda wa miaka kumi na miwili; miaka sita alikuwa anatawala kutoka mjini Tirza. Alinunua mlima wa Samaria kwa vipande 6,000 vya fedha kutoka kwa mtu mmoja aitwaye Shemeri, akajenga ngome juu yake, na mji. Mji wenyewe akauita Samaria, kwa heshima ya Shemeri aliyeumiliki mlima huo hapo awali. Omri alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; alifanya maovu zaidi ya wale wote waliomtangulia. Kwa sababu alimwiga Yeroboamu mwana wa Nebati, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi kwa kuabudu sanamu za miungu. Matendo mengine ya Omri na ushujaa wake, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Hatimaye, Omri alifariki, akazikwa huko Samaria; mwanawe Ahabu akatawala mahali pake. Mnamo mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ahabu mwana wa Omri, alianza kutawala Israeli. Alitawala huko Samaria kwa muda wa miaka ishirini na miwili. Ahabu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kuliko wafalme wote waliomtangulia. Tena, licha ya kuiga mwenendo mbaya wa Yeroboamu mwana wa Nebati, Ahabu alimwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni; akamtumikia na kumwabudu Baali. Alimjengea Baali hekalu huko Samaria, na ndani yake akatengeneza madhabahu ya kumtambikia. Hali kadhalika, alitengeneza sanamu ya Ashera mungu wa kike. Ahabu alitenda maovu mengi, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu Mungu wa Israeli zaidi ya wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. Wakati wa utawala wake, Hieli kutoka Betheli, aliujenga upya mji wa Yeriko. Na sawa kabisa na neno la Mwenyezi-Mungu alilonena kwa njia ya Yoshua mwana wa Nuni, Hieli alifiwa na mzaliwa wake wa kwanza Abiramu, wakati wa kuiweka misingi ya Yeriko, akafiwa pia na mwanawe mdogo Segubu, wakati wa kuyaweka malango yake. Basi Elia wa kijiji cha Tishbe huko Gileadi, akamwambia mfalme Ahabu, “Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli aliye hai ambaye mimi ninamtumikia: Hakutakuwa na umande wala mvua mpaka nitakapotoa amri.” Kisha, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Elia: “Ondoka hapa uelekee mashariki, ukajifiche penye kijito cha Kerithi kilichoko mashariki ya mto Yordani. Huko, utapata maji ya kunywa katika kijito hicho tena nimewaamuru kunguru wakuletee chakula.” Basi, Elia akatii agizo la Mwenyezi-Mungu, akaenda kukaa kwenye kijito cha Kerithi kilichoko mashariki ya mto Yordani. Kunguru wakawa wanamletea mkate na nyama, asubuhi na jioni; akapata na maji ya kunywa katika kijito hicho. Lakini, baada ya siku chache kijito kikakauka kwa sababu hapakunyesha mvua nchini. Hapo, neno la Mwenyezi-Mungu, lilimjia Elia: “Ondoka uende mjini Sarefathi, karibu na Sidoni, ukae huko. Nimemwamuru mwanamke mmoja mjane akupatie chakula huko.” Basi, Elia akaondoka, akaenda Sarefathi. Alipofika penye lango la mji, alimkuta mwanamke mmoja mjane anaokota kuni. Elia akamwita mwanamke huyo na kumwambia “Niletee maji ninywe.” Yule mwanamke alipokuwa anaondoka, Elia akamwita tena na kumwambia, “Niletee na kipande cha mkate pia.” Huyo mwanamke akamwambia, “Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wako aliye hai, sina mkate hata kidogo. Nilicho nacho ni konzi ya unga katika chungu na mafuta kidogo katika chupa. Nimefika hapa kuokota kuni, kisha niende nyumbani kupika chakula hicho, mwanangu na mimi tule, kisha tufe.” Elia akamwambia, “Usiogope. Nenda ukafanye kama ulivyosema. Lakini nitengenezee mimi kwanza na kuniletea andazi dogo, kisha jitengenezee wewe na mwanao chakula. Maana, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Unga ulioko chunguni mwako hautapungua wala mafuta yaliomo ndani ya chupa hayataisha, mpaka hapo mimi Mwenyezi-Mungu nitakaponyesha mvua nchini.’” Basi, huyo mwanamke mjane akaenda akafanya kama alivyoambiwa na Elia hata mama huyo, jamaa yake na Elia wakapata chakula kwa siku nyingi. Unga chunguni haukupunguka, wala mafuta katika chupa hayakwisha sawa kabisa na neno la Mwenyezi-Mungu alilomwambia Elia aseme. Baada ya hayo, mwana wa mwanamke huyo mwenye nyumba akaugua, na hali yake ikazidi kuwa mbaya, hata mwishowe akafariki. Huyo mwanamke akamwambia Elia, “Ewe mtu wa Mungu, una kisa gani nami? Kumbe ulikuja kwangu kuzifichua dhambi zangu na kusababisha kifo cha mwanangu?” Elia akamwambia, “Nipe mwanao.” Basi, Elia akamtwaa mtoto kifuani pa mama yake, akamchukua juu chumbani mwake, akamlaza juu ya kitanda chake. Kisha akamsihi Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, je, hata mwanamke huyu mjane ambaye ninakaa kwake, naye ananitunza, unamletea balaa kwa kumwua mwanawe?” Kisha Elia akajinyosha juu ya mtoto huyo mara tatu na kumwomba Mwenyezi-Mungu, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mrudishie mtoto huyu roho yake!” Mwenyezi-Mungu akasikiliza ombi la Elia; mtoto akaanza kupumua tena. Elia akamrudisha mtoto chini kwa mama yake, akamwambia, “Tazama! Mwanao yu hai.” Huyo mwanamke mjane akamwambia Elia, “Sasa najua kwa hakika kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na maneno aliyokupa Mwenyezi-Mungu uyaseme ni ya kweli.” Ikawa baada ya siku nyingi, mnamo mwaka wa tatu wa ukame, neno hili la Mwenyezi-Mungu likamjia Elia: “Nenda ukajioneshe kwa mfalme Ahabu, halafu nitanyesha mvua nchini.” Basi, Elia akaenda kujionesha kwa Ahabu. Wakati huo, njaa ilikuwa kali sana huko Samaria. Basi, Ahabu akamwita Obadia msimamizi wa ikulu. (Obadia alikuwa mtu amchaye Mwenyezi-Mungu sana, na wakati Yezebeli alipowaua manabii wa Mwenyezi-Mungu, Obadia aliwachukua manabii 100, akawaficha hamsinihamsini pangoni, akawa anawapelekea chakula na maji). Kisha, Ahabu akamwambia Obadia, “Labda tutapata majani na hapo tutawaokoa baadhi ya farasi na nyumbu wetu.” Basi, wakagawana nchi ili wapate kuipitia yote; Ahabu akaenda upande mmoja na Obadia upande mwingine. Obadia alipokuwa njiani, alikutana na Elia; naye Obadia alipomtambua Elia, aliinama chini na kusema, “Kumbe! Ni wewe bwana wangu Elia?” Elia akamwambia, “Naam! Ni mimi Elia. Nenda ukamwambie bwana wako kwamba niko hapa.” Obadia akasema, “Nimekosa nini hata utake kunitia hatarini ili niuawe na mfalme Ahabu? Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wako aliye hai, kwamba mfalme amekuwa akikutafuta duniani kote. Na mfalme yeyote akisema kwamba hujaonekana huko, Ahabu alimtaka huyo mfalme aape na watu wake kwamba kweli hupo. Na sasa, wataka niende kumwambia kwamba wewe uko hapa! Ninahofia kwamba mara nitakapoondoka, Roho ya Mwenyezi-Mungu itakunyakua na kukupeleka mahali nisipopajua! Nikienda kumwambia Ahabu kwamba uko hapa, naye akikutafuta asikupate, ataniua mimi, ingawaje mimi mtumishi wako nimemcha Mwenyezi-Mungu tangu ujana wangu. Je, huna habari kwamba Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Mwenyezi-Mungu, mimi niliwaficha manabii 100, watu hamsinihamsini pangoni, nikawa nawapa chakula na maji? Sasa waniambia ati niende kumwambia bwana wangu kwamba wewe Elia uko hapa! Ahabu ataniua.” Elia akamwambia, “Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa Majeshi, aishivyo ambaye ninamtumikia: Leo hii nitajitokeza mbele ya mfalme.” Basi, Obadia akaenda kwa mfalme Ahabu, akampa habari hizo. Naye Ahabu akaenda kukutana na Elia. Ahabu alipomwona Elia, alisema, “Kumbe kweli ni wewe, mtaabishaji wa Israeli?” Elia akamjibu, “Mtaabishaji wa Israeli si mimi, bali ni wewe na jamaa ya baba yako. Nyinyi mmekiuka amri za Mwenyezi-Mungu na kuabudu Mabaali. Sasa, uwakusanye watu wote wa Israeli mbele yangu huko mlimani Karmeli. Hali kadhalika, wakusanye wale manabii 450 wa Baali, na manabii 400 wa Ashera mungu wa kike, ambao huhifadhiwa na malkia Yezebeli.” Basi, Ahabu akawaita watu wote wa Israeli, akawakusanya na manabii wote kule mlimani Karmeli. Kisha, Elia akawakaribia watu hao, akawaambia, “Mtasitasita na kuyumbayumba mioyoni mpaka lini? Ikiwa Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu mfuateni; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi, mfuateni yeye.” Lakini watu hawakumjibu neno lolote. Hapo, Elia akawaambia, “Mimi tu ndiye peke yangu nabii wa Mwenyezi-Mungu niliyebaki, lakini manabii wa Baali wapo 450. Haya! Leteni fahali wawili; manabii wa Baali wajichagulie fahali mmoja, wamchinje, wamkate vipandevipande na kumweka juu ya kuni, bila kuwasha moto. Nami pia nitamtwaa huyo fahali mwingine, nitamchinja na kumweka juu ya kuni bila kuwasha moto. Kisha, wao watamwomba mungu wao, nami nitamwomba Mwenyezi-Mungu. Mungu atakayejibu kwa kuleta moto, huyo ndiye Mungu wa kweli.” Na hapo umati wote ukasema, “Naam! Na iwe hivyo.” Kisha, Elia akawaambia manabii wa Baali, “Nyinyi ni wengi; basi anzeni. Jichagulieni fahali, mtayarisheni na kumwomba mungu wenu, lakini msiwashe moto.” Hao manabii wakamtwaa fahali wao waliyepewa, wakamtayarisha, kisha wakaanza kumlilia Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakirukaruka na kuyumbayumba kuizunguka madhabahu waliyotengeneza wakisema: “Ee Baali, utusikie!” Lakini hapakutokea sauti yoyote, wala hakuna aliyewajibu. Ilipofika saa sita mchana, Elia akaanza kuwadhihaki akisema, “Ombeni kwa sauti kubwa zaidi! Yeye ni mungu ati! Huenda ikawa amezama katika mawazo yake, amekwenda haja, au yumo safarini! Labda amelala, mnapaswa kumwamsha!” Manabii hao wakapiga kelele zaidi, wakajikatakata kwa visu na simi, kufuatana na desturi yao, hata wakabubujika damu. Wakaendelea kupiga makelele na kufanya kama wendawazimu hadi alasiri wakati wa kutoa tambiko; lakini hakuna aliyewajibu wala kuwajali. Basi, Elia akawaambia watu, “Sogeeni karibu nami.” Wao wakamkaribia. Kisha Elia akaijenga upya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu iliyokuwa imebomolewa. Alitwaa mawe kumi na mawili, hesabu ya makabila kumi na mawili yaliyopewa majina ya wana wa Yakobo ambaye Mwenyezi-Mungu alimwambia “Jina lako litakuwa Israeli.” Kwa mawe hayo, Elia alimjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu, akachimba na mtaro kuizunguka madhabahu hiyo; mtaro uwezao kuchukua kama debe moja na nusu la nafaka. Kisha akapanga kuni vizuri, akamkata vipandevipande yule fahali, akaviweka juu ya kuni. Kisha akawaambia watu, “Jazeni mitungi minne maji mkaimwagie tambiko hii ya kuteketezwa pamoja na kuni.” Wakafanya hivyo. Kisha akawaambia, “Rudieni tena.” Nao wakafanya hivyo mara ya pili. Naye akawaambia, “Fanyeni hivyo tena mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo. Maji yakatiririka chini pande zote za madhabahu, hata yakajaa mtaroni. Mnamo alasiri, wakati wa kutoa tambiko, nabii Elia aliikaribia madhabahu, akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, waoneshe watu leo hii kwamba wewe ndiwe Mungu wa Israeli, na kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya kwa amri yako. Unijibu, ee Mwenyezi-Mungu; unijibu ili watu hawa wajue kuwa wewe Mwenyezi-Mungu ndiwe Mungu, na kwamba umeigeuza mioyo yao wakurudie.” Mara, Mwenyezi-Mungu akashusha moto, ukaiteketeza tambiko hiyo ya kuteketezwa, kuni, mawe na vumbi, na kuyakausha maji yote mtaroni. Watu walipoona hivyo, walianguka kifudifudi na kusema, “Mwenyezi-Mungu, ni Mungu; Mwenyezi-Mungu, ni Mungu!” Ndipo Elia akawaambia, “Wakamateni manabii wote wa Baali. Msimwache hata mmoja wao atoroke!” Basi, watu wakawakamata wote, naye Elia akawapeleka mtoni Kishoni, akawaulia huko. Baada ya hayo, Elia akamwambia mfalme Ahabu, “Nenda ukale na kunywa. Nasikia kishindo cha mvua.” Basi, Ahabu akaenda zake kula na kunywa; naye Elia akapanda juu ya kilele cha mlima Karmeli, na huko akainama hadi chini na kuuweka uso wake katikati ya magoti yake. Kisha akamwambia mtumishi wake, “Sasa, nenda utazame upande wa baharini.” Mtumishi akaenda, akatazama, kisha akarudi akasema, “Hamna kitu.” Elia akamwambia, “Nenda tena mara saba.” Mara ya saba, huyo mtumishi akarudi, akasema, “Naona wingu dogo kama mkono wa mtu linatoka baharini.” Elia akamwambia, “Nenda umwambie mfalme Ahabu atayarishe gari lake la kukokotwa, ateremke, asije akazuiliwa na mvua.” Muda haukupita mrefu mbingu zikatanda mawingu mazito, upepo ukavuma, pakanyesha mvua kubwa. Ahabu naye akapanda gari lake la kukokotwa, akarudi Yezreeli. Nguvu ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Elia, naye akajifunga na kukaza joho lake, akakimbia na kumtangulia Ahabu kuingia mjini Yezreeli. Mfalme Ahabu alimsimulia mkewe Yezebeli mambo yote aliyofanya Elia na jinsi alivyowaua manabii wa Baali kwa upanga. Yezebeli akatuma mjumbe kwa Elia amwambie: “Miungu waniulie mbali, nakuapia, ikiwa saa hizi kesho sitakuwa nimekufanya kama mmoja wa hao manabii.” Elia akakimbilia mjini Beer-sheba mkoani Yuda, alikomwacha mtumishi wake, naye akatembea mwendo wa siku nzima kuingia jangwani. Basi, akafika, akaketi chini ya mti mmoja, mretemu. Hapo, akaomba afe, akisema, “Imetosha! Siwezi tena. Ee Mwenyezi-Mungu, sasa utoe uhai wangu. Mimi si bora kuliko wazee wangu.” Basi, Elia akalala chini ya mti huo, akashikwa na usingizi. Punde, malaika akaja, akamgusa na kumwambia, “Amka ule.” Elia alipotazama, akaona mkate uliookwa juu ya makaa, na chupa ya maji karibu na kichwa chake. Basi, akala, akanywa, akalala tena. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamjia tena mara ya pili, akamgusa na kumwambia, “Amka ule, la sivyo safari itakuwa ngumu mno kwako.” Elia akaamka, akala na kunywa. Kisha akatembea kwa nguvu ya chakula hicho mwendo wa siku arubaini, mchana na usiku, mpaka Horebu, mlima wa Mungu. Huko, akafika penye pango, akakaa humo. Mara neno la Mwenyezi-Mungu likamjia: “Elia! Unafanya nini hapa?” Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda, waniue!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda ukasimame mlimani, mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mwenyezi-Mungu akapita na kuuvumisha upepo mkali ambao uliporomosha milima na kuvunja miamba. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika upepo huo. Upepo ukapita, kukawa na tetemeko la ardhi. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika tetemeko la ardhi. Tetemeko likapita, kukawa na moto. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika moto huo. Baada ya moto, pakatokea sauti ndogo, tulivu. Basi, Elia aliposikia sauti hiyo, alijifunika uso kwa joho lake, akatoka na kusimama mlangoni mwa pango. Hapo, akasikia sauti, “Elia! Unafanya nini hapa?” Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda waniue!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa kupitia njia ya jangwani mpaka Damasko. Utakapofika, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu. Naye Yehu, mwana wa Nimshi, mpake mafuta awe mfalme wa Israeli. Elisha, mwana wa Shafati, wa Abel-mehola, utampaka mafuta awe nabii mahali pako. Basi, yeyote atakayenusurika upanga wa Hazaeli, Yehu atamuua, na yeyote atakayenusurika upanga wa Yehu, Elisha atamuua. Lakini, nitaacha hai watu 7,000 nchini Israeli, ambao hawajamwinamia Baali, wala kuibusu sanamu yake.” Elia akaondoka, akamkuta Elisha, mwana wa Shafati, analima. Hapo, palikuwa na jozi kumi na mbili za ng'ombe wanalima, na jozi ya Elisha ilikuwa ya nyuma kabisa. Basi, Elia akavua joho lake na kumtupia. Hapo, Elisha akawaacha ng'ombe wake, akamfuata Elia mbio na kumwambia, “Niruhusu kwanza niende kumpa baba yangu na mama yangu busu la kwaheri, kisha nikufuate.” Elia akamjibu, “Nenda! Kwani nimekuzuia?” Basi, Elisha akamwacha Elia, akairudia jozi yake ya ng'ombe, akawachinja ng'ombe hao na kuwapika akitumia miti ya nira kama kuni, akawapa watu, wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Elia na kuwa mtumishi wake. Ben-hadadi mfalme wa Aramu, alikusanya jeshi lake lote; aliungwa mkono na wafalme wengine thelathini na wawili pamoja na farasi na magari yao ya kukokotwa. Aliuendea mji wa Samaria akauzingira na kuushambulia. Kisha, akatuma wajumbe wake mjini kwa mfalme Ahabu wa Israeli, wakamwambia, “Mfalme Ben-hadadi asema hivi: ‘Fedha na dhahabu yako yote ni mali yangu; wake zako warembo na watoto wako pia ni wangu.’” Naye mfalme wa Israeli akajibu, “Bwana wangu mfalme, ulivyosema ni sawa: Mimi ni wako, na vyote nilivyo navyo ni vyako.” Baadaye, wajumbe hao wakamrudia tena Ahabu, wakamwambia, “Mfalme Ben-hadadi asema hivi: ‘Nilikutumia ujumbe unipe dhahabu, fedha, wake zako pamoja na watoto wako. Sasa, kesho wakati kama huu, nitatuma watumishi wangu waje kuisaka ikulu na nyumba za watumishi wako, wachukue kila kitu unachothamini.’” Ndipo Ahabu mfalme wa Israeli, akawaita viongozi wote wa nchi, akawaambia, “Sasa, oneni jinsi jamaa huyu anavyotaka kututaabisha! Ametuma ujumbe kwamba anataka wake zangu, watoto wangu, dhahabu na fedha yangu. Nami sikumkatalia!” Wazee na watu wote wakamwambia, “Usimjali wala usikubali.” Basi, Ahabu akawaambia wajumbe wa Ben-hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme hivi: ‘Niko radhi kutimiza matakwa yako ya kwanza, lakini haya ya pili sikubali hata kidogo.’” Hapo, wajumbe hao wakaenda zao na kumhabarisha tena mfalme Ben-hadadi. Ben-hadadi akamtumia Ahabu ujumbe huu: “Miungu na waniulie mbali, nakuapia, ikiwa huko Samaria kutabakia mavumbi ya kutosha gao moja kwa kila mmoja wa watu wangu wengi!” Mfalme Ahabu wa Israeli akajibu, “Mwambieni mfalme Ben-hadadi kwamba shujaa hujisifu baada ya vita, si kabla!” Ben-hadadi alipokea ujumbe huu wa Ahabu wakati yeye na wafalme waliomwunga mkono walipokuwa mahemani mwao wanakunywa. Basi, akayaweka majeshi yake katika hali ya tahadhari, kuushambulia mji. Wakati huohuo, nabii mmoja akamwendea Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Unaona wingi wa majeshi haya? Leo hii nitawatia mikononi mwako, nawe utatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.’” Naye Ahabu akauliza, “Kwa msaada wa nani?” Nabii akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa msaada wa vijana wanaotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya.’” Naye mfalme akauliza, “Ni nani atakayeanza kupigana?” Nabii akajibu, “Wewe!” Basi, mfalme Ahabu akakagua vijana waliotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya, jumla yao watu 232. Kisha akakagua jeshi la Israeli, wanajeshi 7,000. Basi, mnamo adhuhuri, wakati Ben-hadadi na wale wafalme wenzake thelathini na wawili waliomwunga mkono walipokuwa mahemani mwao wakinywa na kulewa, mashambulizi yakaanza. Wale vijana waliotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya, wakatangulia. Wakati huo, Ben-hadadi alikuwa amekwisha peleka askari wa doria, nao wakampa habari kwamba kulikuwa na kundi la watu waliokuja kutoka Samaria. Ben-hadadi akawaambia, “Wakamateni wakiwa hai. Hata kama wanakuja kwa vita au kwa amani.” Basi, wale vijana waliotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya, wakaongoza mashambulizi, huku, nyuma yao, wanafuata wanajeshi wa Israeli. Kila mmoja wao akamuua adui mmoja. Watu wa Aramu wakatimua mbio, nao askari wa Israeli wakawafuatilia; lakini Ben-hadadi, mfalme wa Aramu, akiwa amepanda farasi, akatoroka na baadhi ya askari wapandafarasi. Basi, mfalme wa Israeli akashinda vita, akateka farasi na magari ya kukokotwa mengi, na kuwaua watu wa Aramu kwa wingi. Kisha, yule nabii akamwendea mfalme wa Israeli, akamwambia, “Jiandae upya ufikirie vizuri la kufanya. Mwakani, mfalme wa Aramu atakuja kupambana nawe tena.” Watumishi wa mfalme Ben-hadadi walimshauri hivi: “Miungu ya Waisraeli ni miungu ya milimani; ndiyo maana tulishindwa. Lakini, bila shaka tutawashinda kama tukipigana nao mahali tambarare. Sasa, wastaafishe wale wafalme thelathini na wawili na mahali pao uweke majemadari. Unda jeshi kama lilelile ulilopoteza, farasi na magari ya kukokotwa kama yale uliyopoteza. Kisha, tutapigana nao mahali tambarare na bila shaka tutawazidi nguvu.” Mfalme Ben-hadadi akasikia ushauri wao, akafanya hivyo. Mara baada ya majira ya baridi, mfalme Ben-hadadi aliwakusanya watu wake, akaenda mjini Afeka kupigana na watu wa Israeli. Nao watu wa Israeli walikusanywa na kupewa silaha, wakaenda kuwakabili Waaramu. Watu wa Israeli walipiga kambi, wakaonekana kama vikundi vidogovidogo vya mbuzi, lakini Waaramu walitapakaa kote nchini. Ndipo, mtu mmoja wa Mungu akamkaribia mfalme wa Israeli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa kuwa Waaramu wamesema kwamba mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu wa milimani wala si Mungu wa nchi tambarare, nitakupa ushindi dhidi ya jeshi hili kubwa, nawe utatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.’” Watu wa Israeli na Waaramu walipiga kambi kwa muda wa siku saba, wakikabiliana; siku ya saba, mapigano yakaanza. Siku hiyohiyo, watu wa Israeli wakaua askari wa miguu 100,000. Waliosalia, walikimbilia mjini Afeka. Huko, kuta za mji ziliwaangukia na kuwaua watu 27,000 waliobakia. Ben-hadadi pia alikimbia na kujificha katika chumba fulani cha ndani, mjini. Watumishi wake wakamwendea wakamwambia, “Tumesikia kwamba wafalme wa Israeli ni watu wenye huruma. Basi, turuhusu tujifunge magunia viunoni na kamba shingoni, tumwendee mfalme wa Israeli. Huenda atayasalimisha maisha yako.” Basi, wakajifunga magunia viunoni na kamba shingoni mwao, wakamwendea mfalme wa Israeli, wakamwambia, “Mtumishi wako, Ben-hadadi, anakusihi akisema ‘Tafadhali uniache nipate kuishi.’ Ahabu akasema, ‘Kumbe anaishi bado? Yeye ni ndugu yangu.’” Watumishi wa Ben-hadadi walikuwa wanategea ishara yoyote ile ya bahati njema, basi Ahabu aliposema hivyo, wao wakadakia wakasema, “Naam, Ben-hadadi ni ndugu yako!” Ahabu akawaambia, “Nendeni mkamlete kwangu.” Basi, Ben-hadadi alipomjia, Ahabu akamtaka aketi naye katika gari lake la kukokotwa. Kisha, Ben-hadadi akamwambia, “Miji yote ambayo baba yangu alimnyanganya baba yako, nitakurudishia. Unaweza kuanzisha masoko huko Damasko kama alivyofanya baba yangu huko Samaria.” Ahabu akajibu, “Nitakuachilia kwa masharti hayo.” Hapo, akafanya mkataba naye na kumwacha huru. Kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, mmojawapo wa wanafunzi wa manabii, akamwambia mwenzake, “Nipige, tafadhali.” Lakini mwenzake akakataa kumpiga. Naye akamwambia, “Kwa kuwa umekataa kutii amri ya Mwenyezi-Mungu, basi, mara tu utakapoachana nami, simba atakuua.” Na kweli, mara tu alipoachana naye, akakutana na simba, akamuua. Kisha, huyo mwanafunzi akamkuta mtu mwingine, akamwambia, “Nipige tafadhali.” Mtu huyo akampiga na kumjeruhi. Basi, nabii akaondoka, akaenda akakaa kando ya njia, kumngojea mfalme wa Israeli, huku amejifunga kitambaa usoni, asitambulike. Mfalme alipokuwa anapita, nabii akamlilia akisema, “Bwana, mimi mtumishi wako nilikuwa mstari wa mbele vitani; akaja askari mmoja, akaniletea mateka mmoja na kuniambia, ‘Mlinde mtu huyu; akitoroka utalipa kwa maisha yako wewe binafsi, au kwa vipande 3,000 vya fedha.’ Lakini nilipokuwa nikishughulikashughulika, mtu huyo akatoroka.” Mfalme wa Israeli akamwambia, “Ndivyo itakavyokuwa hukumu yako; umejihukumu mwenyewe.” Hapo, nabii akaondoa harakaharaka kitambaa usoni mwake, naye mfalme akamtambua kuwa mmoja wa manabii. Basi, nabii akamwambia mfalme, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa kuwa umemwachilia mtu ambaye niliamuru auawe akuponyoke, basi, maisha yake utalipa kwa maisha yako, na watu wake kwa watu wako.’” Basi, mfalme wa Israeli akaenda zake nyumbani Samaria, amejaa chuki na huzuni nyingi. Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, alikuwa na shamba lake la mizabibu huko Yezreeli, karibu na ikulu ya Ahabu, mfalme wa Samaria. Basi, siku moja, Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, kwa sababu liko karibu na nyumba yangu. Nitakupa shamba lingine zuri zaidi, au ukitaka, nitakulipa thamani yake, fedha taslimu.” Lakini, Nabothi akamjibu, “Jambo la kukupa wewe urithi nilioupata kwa wazee wangu, Mwenyezi-Mungu na apishe mbali.” Hapo, Ahabu akaenda zake nyumbani amejaa chuki na huzuni nyingi, kwa sababu Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, alimwambia kwamba hatampa kile alichorithi kutoka kwa wazee wake. Basi, akajilaza kitandani, akauficha uso wake na kususia chakula. Yezebeli, mkewe, akamwendea na kumwuliza, “Mbona umejaa huzuni moyoni hata kula huli?” Naye akamwambia, “Kwa sababu nilizungumza na Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, nikamtaka aniuzie shamba lake la mizabibu, ama akipenda nimpe shamba lingine badala ya hilo. Lakini yeye akaniambia, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’” Hapo, Yezebeli, mkewe, akamwambia, “Anayetawala Israeli ni nani? Si ni wewe? Amka, ule na uchangamke; mimi binafsi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli.” Basi, Yezebeli akaandika barua kadha kwa jina la Ahabu na kuzipiga mhuri wa mfalme. Kisha akapeleka barua hizo kwa wazee na watu mashuhuri walioishi na Nabothi huko mjini. Barua zenyewe ziliandikwa hivi: “Pigeni mbiu ya mfungo, mkutane na kumpa Nabothi mahali pa heshima kati ya watu. Kisha, tafuteni walaghai wawili wamkabili na kumshtaki wakisema: ‘Wewe umemwapiza Mungu na mfalme.’ Kisha mtoeni nje, mkamuue kwa kumpiga mawe!” Basi, wakazi wenzake Nabothi, wazee na watu mashuhuri wa mji wa Yezreeli, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza. Kwa mujibu wa barua aliyowapelekea, wakapiga mbiu ya mfungo, wakakutana na kumweka Nabothi mahali pa heshima kati ya watu. Wale walaghai wawili wakaketi kumkabili Nabothi, kisha wakamshtaki hadharani wakisema, “Nabothi amemwapiza Mungu na mfalme.” Basi, Nabothi akatolewa nje ya mji, akauawa kwa kupigwa mawe. Kisha, Yezebeli akapelekewa habari kwamba Nabothi amekwisha uawa kwa kupigwa mawe. Mara tu Yezebeli alipopata habari kwamba Nabothi amekwisha uawa kwa kupigwa mawe, akamwambia Ahabu, “Inuka! Nenda ukamiliki lile shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Nabothi hayuko hai tena; amekwisha fariki.” Mara tu Ahabu aliposikia Nabothi amekwisha fariki, aliinuka kwenda kulimiliki shamba la mizabibu la Nabothi. Basi, neno la Mwenyezi-Mungu likamjia nabii Elia wa Tishbe: “Inuka uende kukutana na Ahabu mfalme wa Israeli, ambaye yuko Samaria. Utamkuta katika shamba la mizabibu la Nabothi, akilimiliki. Mwambie, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Umeua na kumiliki pia?’ Mwambie Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, ndipo watakapoilamba damu yako.’” Basi, Ahabu alipomwona Elia, akasema, “Ewe adui yangu, umenifuma?” Elia akamjibu, “Naam! Nimekufuma, kwa sababu wewe umenuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Haya! Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Hakika, nitakuletea maangamizi. Nitakuzoa wewe na kufutilia mbali kila mwanamume wa ukoo wako katika Israeli, awe mtumwa au huru. Jamaa yako nitaifanya kama jamaa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kama jamaa ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umeiwasha hasira yangu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.’ Tena, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Yezebeli: ‘Mbwa wataula mwili wa Yezebeli humuhumu mjini Yezreeli. Naam, yeyote wa jamaa yake atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla.’” (Hakuna mtu aliyenuia kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama Ahabu, ambaye alishawishiwa na Yezebeli, mkewe. Alitenda machukizo kwa kuabudu sanamu za miungu kama walivyofanya Waamori ambao hapo awali Mwenyezi-Mungu aliwafukuza mbele ya watu wa Israeli). Lakini, Ahabu aliposikia maneno hayo, alirarua nguo zake, akajivalia gunia peke yake, akafunga, akawa analala na gunia, na kwenda huko na huko kwa huzuni. Basi, ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu ukamjia Elia wa Tishbe: “Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekesha mbele yangu? Basi, kwa kuwa amejinyenyekesha, sitaleta yale maangamizi akiwa hai, lakini nyakati za utawala wa mwanawe nitaiangamiza jamaa yake Ahabu.” Kwa muda wa miaka mitatu hivi, kulikuwa na amani kati ya Israeli na Aramu. Lakini mnamo mwaka wa tatu, Yehoshafati, mfalme wa Yuda, alifika kumtembelea Ahabu, mfalme wa Israeli. Ahabu akawaambia watumishi wake, “Je, hamjui kwamba Ramoth-gileadi ni mali yetu? Mbona basi tunajikalia tu bila kuunyakua kutoka kwa mfalme wa Aramu?” Kisha akamwambia Yehoshafati, “Je, utaandamana nami kupigana huko Ramoth-gileadi?” Naye Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Naam; mimi na wewe ni kitu kimoja, na pia watu wangu ni watu wako, farasi wangu ni farasi wako.” Kisha Yehoshafati aliendelea kumwambia mfalme wa Israeli: “Lakini, kwanza mwulize Mwenyezi-Mungu ushauri.” Basi, Ahabu akaitisha kikao cha manabii wapatao 400, akawauliza, “Je, niende nikaushambulie mji wa Ramoth-gileadi au nisiende?” Wao wakamjibu: “Nenda! Mwenyezi-Mungu atakupatia ushindi.” Lakini, Yehoshafati akasema, “Je, hapa hakuna nabii mwingine wa Mwenyezi-Mungu ambaye twaweza kumwuliza shauri?” Naye mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Yupo, bado mmoja, Mikaya mwana wa Imla. Yeye twaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu. Lakini namchukia sana kwa sababu yeye, kamwe hatabiri jambo jema juu yangu, ila mabaya tu.” Yehoshafati akamwambia, “Si vizuri mfalme kusema hivyo.” Basi, Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwita mtumishi mmoja, akamwamuru, “Haraka! Nenda ukamlete Mikaya mwana wa Imla.” Wakati huo, mfalme wa Israeli pamoja na Yehoshafati mfalme wa Yuda, walikuwa wameketi katika viti vyao vya enzi wakikaa kwenye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la kuingilia mjini Samaria nao walikuwa wamevalia mavazi yao ya kifalme; wakati huo manabii wote wakawa wanatabiri mbele yao. Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Waaramu na kuwaangamiza.’” Hata wale manabii wengine wote wakatabiri vivyo hivyo, wakasema, “Nenda uushambulie Ramoth-gileadi, utashinda! Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.” Wakati huo, yule mtumishi aliyetumwa kwenda kwa Mikaya, alimwambia, “Manabii wengine wote kwa pamoja, wamemtabiria mfalme ushindi; tafadhali, nawe pia ufanye kama wao, umtabirie mema.” Lakini Mikaya akamjibu, “Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, mimi nitasema tu yale atakayoniambia Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mikaya alipofika mbele ya mfalme, mfalme alimwuliza, “Je, twende kupigana vita huko Ramoth-gileadi ama tusiende?” Naye alimjibu, “Nenda na ufanikiwe, naye Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.” Lakini mfalme akamwambia, “Nitakuapisha mara ngapi kwamba unaposema nami kwa jina la Mwenyezi-Mungu, ni lazima uniambie ukweli mtupu?” Ndipo, Mikaya akasema, “Niliona watu wote wa Israeli wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji. Naye Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi; basi warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.’” Hapo, mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kamwe hatatabiri jema juu yangu ila mabaya tu?” Kisha Mikaya akasema, “Haya sikia neno la Mwenyezi-Mungu: Nilimwona Mwenyezi-Mungu ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni limesimama kando yake, upande wake wa kulia na wa kushoto; ndipo Mwenyezi-Mungu akauliza, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu aende akaangamie huko Ramoth-gileadi?’ Kila mmoja akajibu alivyofikiri. Kisha pepo mmoja akajitokeza mbele ya Mwenyezi-Mungu, akasema, ‘Mimi nitamshawishi.’ Mwenyezi-Mungu akamwuliza, ‘Kwa mbinu gani?’ Naye akajibu, ‘Nitakwenda na kuwafanya manabii wake wote waseme uongo.’ Mwenyezi-Mungu akamwambia, ‘Wewe utamshawishi na utafaulu; haya, nenda ukafanye hivyo.’ Basi, ndivyo ilivyo: Mwenyezi-Mungu amewafanya hawa manabii wako wote waseme uongo. Mwenyezi-Mungu amenena mabaya juu yako!” Hapo, Sedekia, mwana wa Kenaana, akamkaribia Mikaya, akampiga kofi shavuni na kumwuliza, “Tangu lini Roho ya Mwenyezi-Mungu ikaniacha mimi, ikaja kunena nawe?” Mikaya akamjibu, “Siku utakapoingia katika chumba cha ndani kujificha, ndipo utakapojua.” Naye mfalme wa Israeli akatoa amri, “Mkamateni Mikaya; mrudisheni kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme. Waambie wamtie gerezani na kumlisha mkate kidogo na maji, mpaka nitakaporudi salama.” Ndipo Mikaya aliposema, “Ukirudi salama basi, utajua kwamba Mwenyezi-Mungu hakunena nami.” Kisha akaendelea kusema, “Sikilizeni enyi watu wote!” Basi, mfalme wa Israeli akaenda pamoja na mfalme Yehoshafati wa Yuda, kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Mimi nitavaa mavazi yasiyo ya kifalme na kuingia vitani lakini wewe utavaa mavazi yako ya kifalme.” Hivyo mfalme wa Israeli akaenda vitani bila kuvaa mavazi ya kifalme. Mfalme wa Aramu alikuwa amewaamuru makapteni wake thelathini na wawili waliosimamia magari yake ya kukokotwa, akisema: “Msipigane na mtu yeyote yule, mkubwa au mdogo, ila tu na mfalme wa Israeli.” Baadaye, makapteni hao walipomwona Yehoshafati, walisema: “Kweli, huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo, walimwelekea, wakamshambulia; lakini Yehoshafati akapiga kelele. Makapteni walipotambua kwamba hakuwa mfalme wa Israeli waliacha kumshambulia, wakarudi. Lakini, askari mmoja wa Aramu, akauvuta upinde wake kwa kubahatisha, mshale ukamchoma mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma kifuani. Ahabu akamwambia dereva wa gari lake, “Geuza gari uniondoe vitani. Nimejeruhiwa!” Na mapigano siku hiyo yakazidi kuwa makali, huku mfalme ameegemeshwa garini, anawaelekea watu wa Aramu. Ilipofika jioni, akafariki. Damu ikawa inamtoka jerahani mwake na kutiririka hadi chini ya gari. Mnamo machweo ya jua, amri ikatolewa: “Kila mtu arudi mjini kwake; kila mtu arudi nchini kwake!” Mfalme Ahabu alipofariki maiti yake ilipelekwa Samaria, ikazikwa huko. Gari lake la kukokotwa waliliosha katika bwawa la Samaria, mbwa wakairamba damu yake, nao makahaba wakaoga humo, sawa kabisa na neno alilosema Mwenyezi-Mungu. Matendo mengine ya mfalme Ahabu, jinsi alivyojenga na kupamba nyumba yake kwa pembe, na miji yote aliyojenga, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Ahabu alipofariki, mwanawe Ahazia alitawala mahali pake. Mnamo mwaka wa nne wa utawala wa mfalme Ahabu wa Israeli, Yehoshafati mwana wa Asa, alianza kutawala Yuda. Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala. Alitawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na mitano. Mama yake alikuwa Azuba binti Shilhi. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyofanya baba yake Asa. Lakini hakupaharibu mahali pa kutambikia vilimani. Watu waliendelea kutambikia na kufukiza ubani mahali hapo. Yehoshafati pia, alifanya mapatano ya amani na mfalme wa Israeli. Matendo mengine ya Yehoshafati, ushujaa wake na vita alivyopigana, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Wafiraji wote wa kidini waliosalia tangu nyakati za baba yake Asa, Yehoshafati aliwaondoa nchini. Katika nchi ya Edomu, hapakuwa na mfalme. Nchi hiyo ilitawaliwa na naibu. Mfalme Yehoshafati aliunda meli za kwenda Ofiri kuleta dhahabu lakini hazikufika kwa sababu zilivunjikavunjika huko Esion-geberi. Basi, Ahazia mwana wa Ahabu, akamwambia Yehoshafati, “Waache watumishi wangu wasafiri pamoja na watumishi wako katika meli.” Lakini Yehoshafati hakukubali jambo hilo. Hatimaye, Yehoshafati alifariki, na kuzikwa pamoja na babu zake katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi baba yake; naye Yehoramu, mwanawe, akatawala mahali pake. Mnamo mwaka wa kumi na saba wa utawala wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda, Ahazia, mwana wa Ahabu, alianza kutawala Israeli. Alitawala kwa muda wa miaka miwili, kutoka Samaria. Ahazia alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; aliuiga mwenendo wa baba yake na mwenendo wa Yezebeli, mama yake, na wa Yeroboamu, mwana wa Nebati ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Alimtumikia na kumwabudu Baali, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kila jambo kama alivyofanya baba yake. Baada ya kifo cha Ahabu, watu wa Moabu waliasi wasitawaliwe na Israeli. Mfalme Ahazia alipokuwa Samaria alianguka kutoka chumba kilichokuwa paani mwa nyumba yake, akaumia vibaya. Kwa hiyo akawatuma wajumbe, akawaambia, “Nendeni kwa Baal-zebubu, mungu wa mji wa Ekroni, mkamwulize kama nitapona ugonjwa huu.” Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia nabii Elia kutoka Tishbe, aende kukutana na wajumbe hao na kuwauliza, “Kwa nini mnakwenda kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Je, hakuna Mungu nchini Israeli? Mwambieni mfalme kwamba Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Hutashuka katika kitanda ulichokipanda; hakika utakufa!’” Basi, Elia akawaendea. Wale wajumbe wakarudi kwa mfalme, naye akawauliza, “Mbona mmerudi?” Wakamjibu, “Tumekutana na mtu ambaye alitutuma turudi kukuambia kwamba Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Kwa nini unatuma wajumbe kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Je, hakuna Mungu nchini Israeli? Hutashuka katika kitanda ulichokipanda; bali hakika utakufa!’” Mfalme akauliza, “Ni mtu gani huyo aliyekutana nanyi na kuwaambieni mambo hayo?” Wao wakamjibu, “Alikuwa amevaa vazi la manyoya na mshipi wa ngozi kiunoni.” Mfalme akasema, “Huyo ni Elia kutoka Tishbe!” Hapo mfalme akamtuma kapteni mmoja na watu wake hamsini wamlete Elia. Kapteni huyo akamkuta Elia ameketi mlimani, akamwambia, “Ewe mtu wa Mungu, mfalme anakuamuru ushuke.” Elia akamjibu huyo kapteni wa watu hamsini, “Kama mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni na kukuteketeza wewe pamoja na watu wako!” Mara moto ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na watu wake hamsini. Mfalme akamtuma kapteni mwingine na watu wake hamsini wamlete Elia. Naye akapanda juu akamwambia Elia, “Ewe mtu wa Mungu, mfalme anakuamuru ushuke mara moja!” Elia akamjibu, “Kama kweli mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe pamoja na watu wako!” Papo hapo moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na watu wake hamsini. Kwa mara nyingine tena, mfalme akatuma kapteni mwingine na watu wake hamsini. Kapteni wa tatu akapanda mlimani, akapiga magoti mbele ya Elia na kumsihi akisema, “Ewe mtu wa Mungu, nakusihi uyathamini maisha yangu, na ya watu wako hawa, usituangamize! Maofisa wawili waliotangulia na watu wao, wameteketezwa na moto ulioshuka kutoka mbinguni; lakini sasa nakuomba uyahurumie maisha yangu.” Hapo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Elia, “Shuka pamoja naye, wala usimwogope.” Basi, Elia akainuka, akashuka pamoja naye mpaka kwa mfalme, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa sababu ulituma wajumbe kumtaka shauri Baal-zebubu, mungu wa Ekroni — kana kwamba hapakuwa na Mungu katika Israeli ambaye ungemwomba shauri — basi, hutashuka katika kitanda ulichopanda; hakika utakufa.’” Baadaye Ahazia akafariki kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia nabii wake Elia. Na, kwa kuwa Ahazia hakuwa na mtoto wa kiume, Yoramu akawa mfalme mahali pake, katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda. Mambo mengine aliyoyatenda mfalme Ahazia, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Ikawa wakati ulipofika ambapo Mwenyezi-Mungu alitaka kumchukua Elia mbinguni katika upepo wa kisulisuli, Elia na Elisha walikuwa njiani, wakitoka Gilgali. Baadaye walipokuwa njiani, Elia alimwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende Betheli.” Lakini Elisha akamwambia, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo, sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja hadi Betheli. Wanafunzi wa manabii waliokuwa huko wakamwendea Elisha, wakamwuliza, “Je, unajua kwamba leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.” Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende Yeriko.” Lakini Elisha akakataa akisema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja mpaka Yeriko. Wanafunzi wa manabii huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumwuliza, “Je, unajua kwamba hivi leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akawajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.” Kisha Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende mtoni Yordani.” Lakini Elisha akasema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja. Manabii hamsini wakawafuata mpaka mtoni Yordani. Elia na Elisha wakasimama karibu na mto, nao manabii wakasimama mbali kidogo. Elia akalivua vazi lake, akalikunja na kuyapiga maji, maji yakagawanyika katika sehemu mbili, nao wakavuka hadi ngambo ya pili, wakapitia mahali pakavu. Walipofika ngambo, Elia akamwambia Elisha, “Niambie unalotaka nikufanyie kabla sijaondolewa kwako.” Elisha akamwambia, “Naomba sehemu maradufu ya roho yako.” Elia akajibu, “Ombi lako ni gumu, hata hivyo utakipokea kipawa changu hicho ikiwa utaniona wakati nitakapoondolewa kwako; lakini usiponiona, basi hutapewa.” Walipokuwa wanatembea na kuongea, ghafla, gari la moto likatokea pamoja na farasi wa moto; likawatenganisha; naye Elia akachukuliwa mbinguni katika kisulisuli. Elisha alipoona tukio hilo akalia, “Baba yangu, baba yangu! Gari la Israeli na wapandafarasi wake!” Basi, Elisha hakumwona tena Elia. Ndipo Elisha alipoyashika mavazi yake na kuyararua vipande viwili. Kisha akaliokota vazi la Elia lililomwangukia, akarudi na kusimama ukingoni mwa mto Yordani. Akayapiga maji kwa vazi la Elia akisema, “Yuko wapi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Elia?” Alipoyapiga maji, yakagawanyika sehemu mbili, naye akavuka hadi ngambo. Wale wanafunzi wa manabii kutoka Yeriko walipomwona, walisema, “Roho ya Elia iko kwa Elisha.” Basi, wakaenda kumlaki, wakasujudu mbele yake. Wakamwambia, “Sisi watumishi wako tunao mashujaa hamsini; tafadhali waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Ikiwa roho ya Mwenyezi-Mungu imembeba na kumtupa juu ya mlima fulani au bondeni.” Elisha akajibu, “La, msiwatume.” Lakini wao waliposisitiza mpaka akaona haya, aliwaambia “Watumeni.” Hivyo wakawatuma watu hamsini, wakaenda wakamtafuta kila mahali kwa muda wa siku tatu wasimwone. Kisha wakarudi kwa Elisha aliyekuwa anawangojea huko Yeriko. Elisha akawauliza, “Je, sikuwaambieni msiende?” Baadaye watu wa Yeriko walimwendea Elisha, wakamwambia, “Bwana, kama uonavyo mji huu ni mzuri, lakini maji tuliyo nayo ni mabaya na yanasababisha mimba kuharibika.” Elisha akawaambia, “Tieni chumvi ndani ya bakuli jipya, kisha mniletee.” Nao wakamletea. Elisha akaenda kwenye chemchemi ya maji, akatupa chumvi hiyo ndani na kusema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimeyafanya maji haya kuwa yenye kufaa; tangu sasa hayatasababisha vifo au kutoa mimba.” Na maji hayo yamekuwa ya kufaa mpaka leo, kama alivyosema Elisha. Elisha aliondoka Yeriko, akaenda Betheli. Alipokuwa njiani, vijana fulani walitoka mjini wakaanza kumzomea wakisema, “Nenda zako, nenda zako mzee kipara!” Elisha aligeuka akawatazama na kuwalaani kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Dubu wawili majike wakatoka mwituni, wakawararua vijana arubaini na wawili miongoni mwao. Elisha akaendelea na safari yake mpaka mlima Karmeli na kutoka huko akarudi Samaria. Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yehoshafati wa Yuda, Yoramu mwana wa Ahabu alianza kutawala Israeli, akatawala kutoka Samaria kwa muda wa miaka kumi na miwili. Yoramu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini yeye hakuwa mbaya kama baba na mama yake; maana alibomolea mbali mnara wa Baali uliofanywa na baba yake. Hata hivyo, Yoramu hakuacha dhambi kama mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati aliyemtangulia ambaye alifanya dhambi na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Mfalme Mesha wa Moabu alikuwa mfuga kondoo, na kila mwaka alitoa ushuru kwa mfalme wa Israeli wanakondoo laki moja na sufu ya kondoo laki moja. Lakini Ahabu alipofariki, mfalme wa Moabu alimwasi. Kwa hiyo mfalme Yoramu akaondoka Samaria, akakusanya jeshi lote la Israeli. Akatuma ujumbe kwa mfalme Yehoshafati wa Yuda, akamwambia, “Mfalme wa Moabu ameniasi. Je, utashirikiana nami tupigane naye?” Mfalme Yehoshafati akamjibu, “Niko tayari! Mimi na wewe ni kitu kimoja; watu wangu ni kama wako, farasi wangu ni kama wako. Je, tutashambulia kutoka upande gani?” Yoramu akajibu, “Tutashambulia kutoka jangwa la Edomu.” Basi, mfalme Yoramu akaondoka pamoja na mfalme wa Yuda na mfalme wa Edomu. Baada ya kusafiri kwa muda wa siku saba, maji yakawaishia. Hawakuwa na maji kwa majeshi yao wala kwa wanyama wao. Hapo mfalme wa Israeli akasema, “Ole wetu! Mwenyezi-Mungu ametukusanya sote wafalme watatu atutie mikononi mwa mfalme wa Moabu.” Mfalme Yehoshafati akauliza, “Je, hakuna nabii yeyote hapa wa Mwenyezi-Mungu ambaye tunaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu?” Mtumishi mmoja wa mfalme Yoramu wa Israeli akajibu, “Elisha mwana wa Shafati yupo hapa. Yeye alikuwa mtumishi wa Elia.” Yehoshafati akasema, “Huyo ni nabii wa kweli.” Kisha wafalme hao watatu wakamwendea Elisha. Elisha akamwuliza mfalme wa Israeli, “Nina uhusiano gani nawe? Nenda ukawatake shauri manabii ambao baba yako na mama yako waliwaendea.” Mfalme wa Israeli akajibu, “Sivyo! Mwenyezi-Mungu ndiye aliyetuita sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa mfalme wa Moabu.” Elisha akasema, “Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu ambaye mimi ninamtumikia, naapa kwamba kama isingekuwa kwa heshima niliyo nayo kwa rafiki yako mfalme Yehoshafati wa Yuda, nisingekujali hata kidogo. Lakini sasa niletee mpiga kinanda.” Wakamletea mpiga kinanda. Ikawa alipopiga kinanda, nguvu ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Elisha, akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Chimbeni mashimo kila mahali kote bondeni. Ingawa hamtaona upepo wala mvua, bonde litajaa maji, nanyi mtakunywa, nyinyi pamoja na ng'ombe wenu na wanyama wenu.’ Lakini hili si jambo gumu kwa Mwenyezi-Mungu; yeye atawapeni pia ushindi juu ya Moabu. Mtashinda kila mji wenye ngome na kila mji mzuri; mtaikata miti yao yote, mtaziba chemchemi zote za maji, na kuyaharibu mashamba yao yote yenye rutuba kwa kuyajaza mawe.” Kesho yake asubuhi, wakati wa kutambikia, maji yakatiririka kutoka upande wa Edomu na kujaa kila mahali bondeni. Wamoabu walipopata habari kwamba hao wafalme watatu wamekuja kuwashambulia, watu wote wawezao kuvaa silaha kuanzia vijana mpaka wazee, waliitwa, wakapewa silaha na kuwekwa mpakani tayari kwa vita. Walipoamka asubuhi iliyofuata, jua lilikuwa linametameta juu ya maji hayo; walipoyatazama yakaonekana kuwa mekundu kama damu. Wakasema, “Hii ni damu! Bila shaka hawa wafalme watatu wamepigana wao kwa wao na kuuana! Twendeni tukachukue nyara!” Lakini walipofika katika kambi ya Israeli, watu wa Israeli waliwashambulia, nao wakakimbia mbele yao. Watu wa Israeli wakawafuatia mpaka Moabu huku wakiwaua na kuibomoa miji yao. Kila walipopita penye shamba zuri, kila mtu alilirushia jiwe mpaka kila shamba likajaa mawe; kadhalika wakaziziba chemchemi zote za maji na kukata miti yote mizuri. Hatimaye, ukabaki mji mkuu wa Kir-haresethi peke yake, ambao pia wapiga kombeo waliuzingira na kuuteka. Mfalme wa Moabu alipoona kwamba vita vinamwendea vibaya, alichukua watu wake 700 wenye kupigana kwa mapanga, akikusudia kupenya majeshi ya adui zake mkabala na mfalme wa Edomu, lakini hakufaulu. Hapo akamchukua mwanawe wa kwanza ambaye angekuwa mfalme mahali pake, akamtoa kuwa sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Watu wa Israeli walipoona hayo, wakachukizwa mno. Wakauacha mji huo na kurudi nchini kwao. Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wanafunzi wa manabii akamwendea Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu amefariki, na kama ujuavyo, alikuwa mcha Mungu, lakini aliyemwia fedha amekuja kuwatwaa wanangu wawili wawe watumwa wake.” Elisha akamwuliza, “Sasa nikusaidieje? Niambie kile ulicho nacho nyumbani.” Mama huyo mjane akamjibu, “Mimi mtumishi wako sina kitu chochote ila chupa ndogo ya mafuta.” Elisha akamwambia, “Nenda kwa jirani zako uazime vyombo vitupu vingi kadiri utakavyopata. Kisha uende, wewe pamoja na wanao, mjifungie ndani ya nyumba, na muanze kujaza mafuta. Kila chombo mnachojaza, kiwekeni kando.” Akaenda na kujifungia ndani ya nyumba na wanawe na kuanza kumimina mafuta ndani ya vyombo. Vilipojaa vyote, akamwambia mwanawe mmojawapo, “Niletee chombo kingine.” Mwanae akamjibu, “Vyote vimejaa!” Hapo mafuta yakakoma kutiririka. Akarudi kwa mtu wa Mungu na kumweleza habari hizo. Naye mtu wa Mungu akamwambia, “Nenda ukauze hayo mafuta na kulipa madeni yako, ndipo wewe na wanao mtaishi kwa kutumia hayo yatakayobaki.” Siku moja Elisha alikwenda Shunemu, ambako alikaa mama mmoja tajiri. Mama huyu akamwalika Elisha kwa chakula, na toka siku hiyo ikawa kawaida Elisha kula chakula kwake kila alipopitia huko. Mama huyo akamwambia mumewe, “Sina shaka kwamba mtu huyu anayefika kwetu kila mara ni mtakatifu wa Mungu. Mbona basi tusimjengee chumba na huko tumwekee kitanda, meza, kiti na taa, ili akitumie kila anapotutembelea?” Siku moja Elisha akaja huko na kuingia chumbani mwake ili apumzike. Akamwuliza mtumishi wake Gehazi, “Mwite huyu mama Mshunami.” Alipomwita alikuja na kusimama mbele yake. Naye Elisha akamwambia Gehazi, “Mwambie, tumeona jinsi alivyotushughulikia; sasa anataka tumtendee jambo gani? Je, angependa aombewe lolote kwa mfalme au kwa jemadari wa jeshi?” Mama Mshunami akamjibu, “Mimi ninaishi miongoni mwa watu wangu.” Elisha akasema, “Tumfanyie nini basi?” Gehazi akamjibu, “Hakika hana mtoto, na mumewe amekuwa mzee.” Elisha akamwambia, “Mwite.” Naye akamwita. Akaja na kusimama mlangoni. Elisha akamwambia “Majira kama haya mwakani, utakapotimia mwaka ujao, wakati kama huu, utakuwa na mtoto mikononi mwako.” Mama akamjibu, “La, Bwana wangu! Wewe ni mtu wa Mungu; usinidanganye mimi mtumishi wako!” Lakini huyo mwanamke akapata mimba na kuzaa mtoto wakati kama huo mwaka uliofuata, kama Elisha alivyokuwa amemwambia. Mtoto huyo alipokua, alitoka siku moja pamoja na baba yake akafuatana na wavunaji, naye akamwambia baba yake, “Ole, kichwa changu! Naumwa na kichwa!” Baba yake akamwambia mtumishi wake mmoja, “Mpeleke kwa mama yake.” Alipofikishwa kwa mama yake, alikaa juu ya magoti ya mama yake mpaka adhuhuri, halafu akafa. Mama yake akampeleka na kumlaza kitandani mwa mtu wa Mungu, akaufunga mlango na kuondoka. Akamwita mumewe na kumwambia, “Nipe mtumishi mmoja na punda mmoja, ili nimwendee mara moja yule mtu wa Mungu, kisha nitarudi.” Mumewe akamwuliza, “Mbona unataka kumwona leo? Leo si siku ya mwezi mwandamo wala Sabato?” Akamjibu, “Usijali.” Akatandika punda na kumwambia mtumishi, “Sasa kaza mwendo, wala usipunguze mpaka nitakapokuambia.” Basi, akaondoka, akaenda mpaka mlima Karmeli alipokuwa mtu wa Mungu. Mtu wa Mungu alipomwona akija, akamwambia Gehazi mtumishi wake, “Tazama, namwona Mshunami akija; kimbia mara moja ukakutane naye na kumwambia, ‘Hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto hajambo?’” Naye Mshunami akamjibu “Hatujambo.” Alipofika mlimani kwa mtu wa Mungu akamshika miguu, naye Gehazi akakaribia ili amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia, “Mwache, kwani ana uchungu mkali, naye Mwenyezi-Mungu hakunijulisha jambo hilo.” Huyo mama akamwambia, “Bwana wangu, je, si nilikuomba mtoto? Kwani sikukusihi usije ukanipa matumaini ambayo yangenipa huzuni baadaye?” Elisha akamwambia Gehazi, “Chukua fimbo yangu, uondoke mara moja. Usisimame njiani kumwamkia mtu yeyote, na mtu yeyote akikuamkia njiani, usipoteze wakati kurudisha salamu. Nenda moja kwa moja mpaka nyumbani na kuweka fimbo yangu juu ya mtoto.” Mwanamke akamwambia Elisha, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe uishivyo, sitakuacha.” Basi Elisha akaondoka na kufuatana naye. Gehazi akatangulia mbele, na alipofika akaweka fimbo ya Elisha juu ya uso wa mtoto, lakini hakukuonekana dalili yoyote ya uhai. Akarudi na kukutana na Elisha, akamwambia, “Kijana hakufufuka.” Elisha alipofika, akaingia peke yake chumbani na kuona maiti ya kijana kitandani. Basi, akafunga mlango na kumwomba Mwenyezi-Mungu. Ndipo akajilaza juu ya mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, na macho yake juu ya macho ya mtoto na mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Na alipokuwa amekaa hivyo, mwili wa mtoto ukaanza kupata joto. Elisha akasimama na kutembeatembea chumbani, kisha akarudi na kujilaza tena juu ya mtoto. Mtoto akapiga chafya mara saba, halafu akafungua macho. Elisha akamwita Gehazi na kumwambia, “Mwite yule Mshunami.” Alipoitwa Elisha akamwambia, “Mchukue mwanao.” Akainama miguuni pa Elisha kwa shukrani na kumchukua mwanawe. Elisha akarudi Gilgali wakati nchini kulikuwa na njaa. Siku moja, alipokuwa akifundisha wanafunzi wa manabii alimwambia mtumishi wake, “Weka chungu kikubwa motoni, uwapikie manabii.” Mmoja wao akaenda shambani na kuchuma mboga. Huko akaona mtango-mwitu, akachuma matango mengi kadiri alivyoweza kuchukua. Akaja nayo, akayakatakata na kuyatia chunguni bila kuyajua. Chakula kikapakuliwa. Lakini walipokionja wakamlilia Elisha wakisema, “Ee mtu wa Mungu, chakula hiki kitatuua!” Nao hawakuweza kukila. Elisha akaagiza aletewe unga. Akaletewa unga, naye akautia ndani ya chungu na kusema, “Sasa wape chakula wale.” Wakakila, na hapo hakikuwadhuru. Mtu Mmoja akatoka Baal-shalisha, akamletea Elisha mikate ishirini iliyotengenezwa kwa shayiri ya malimbuko ya mavuno ya mwaka huo na masuke mabichi ya ngano guniani. Elisha akamwagiza Gehazi awape watu wale. Mtumishi wake akasema, “Sitawapa kwa sababu hakitawatosha watu 100”. Elisha akasema, “Wape wale, kwa sababu Mwenyezi-Mungu amesema kwamba watakula washibe na kingine kitabaki.” Mtumishi wake akawaandalia chakula, wakala wote wakashiba, na kingine kikabaki, kama Mwenyezi-Mungu alivyosema. Naamani, kamanda wa jeshi la mfalme wa Aramu alikuwa mtu mashuhuri aliyependwa sana na bwana wake, kwani kwa njia yake Mwenyezi-Mungu aliiletea nchi ya Aramu ushindi. Alikuwa askari hodari, lakini alikuwa na ugonjwa wa ukoma. Katika vita walivyokuwa wakipigana na Israeli, Waaramu walikuwa wamemchukua msichana mmoja mdogo kutoka Israeli, naye akawa anamtumikia mke wa Naamani. Siku moja akamwambia bibi yake, mke wa Naamani, “Laiti bwana wangu angekwenda na kumwona yule nabii aliyeko Samaria! Angemponya ugonjwa wake.” Naamani alipopata habari hizi, akaenda kwa mfalme na kumweleza habari za mtoto huyu. Mfalme wa Aramu akamwambia, “Chukua barua hii umpelekee mfalme wa Israeli.” Hivyo Naamani akaondoka, huku amechukua vipande 30,000 vya fedha, vipande 6,000 vya dhahabu na mavazi kumi ya sikukuu. Barua yenyewe iliandikwa hivi, “Barua hii ni ya kumtambulisha kwako ofisa wangu Naamani. Nataka umtibu huu ugonjwa wake.” Mfalme wa Israeli aliposoma barua hii alirarua mavazi yake na kusema, “Mbona mfalme wa Aramu anataka nimtibu mtu huyu ukoma wake? Kwani anafikiri mimi ni Mungu aliye na uwezo wa kuua au kufufua? Fahamuni basi, mwone ya kwamba mtu huyu anataka kuniletea mzozo.” Elisha, nabii wa Mungu, alipopata habari kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, alituma ujumbe kwa mfalme, akamwuliza, “Mbona umeyararua mavazi yako? Mlete mtu huyo kwangu, ili apate kujua kwamba kuna nabii katika Israeli?” Naamani akaenda na farasi wake na gari lake mpaka mlangoni mwa Elisha. Elisha akamtuma mtumishi wake amwambie, “Nenda ukaoge mara saba mtoni Yordani, nawe utapona kabisa.” Lakini Naamani alikasirika sana, akaenda zake akisema, “Nilidhani kwamba hakika atanijia na kumwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, apitishe mikono yake juu ya mahali ninapougua na kuniponya! Isitoshe, je, mito Abana na Farpari ya huko Damasko si bora kuliko mito yote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga humo na kupona?” Akaondoka na kurudi nyumbani, huku amekasirika sana. Watumishi wake wakamwendea na kumwambia, “Baba yetu kama nabii angekuambia ufanye jambo fulani gumu, je, hungelifanya? Sasa, aliyokuambia tu ni: ‘Jioshe, ili upone!’” Basi, Naamani akateremka mtoni Yordani akajitumbukiza humo mara saba, kama alivyoagizwa na Elisha mtu wa Mungu, naye akapona kabisa. Ngozi yake ikawa imara na yenye afya kama ya mtoto mdogo. Ndipo akarudi kwa mtu wa Mungu pamoja na watu wake, akasema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu yeyote ila tu Mungu wa Israeli; kwa hiyo, tafadhali sasa upokee zawadi za mtumishi wako.” Elisha akajibu, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai ambaye ninamtumikia, kwamba sitapokea zawadi yoyote.” Naamani akamsihi, lakini Elisha akakataa kabisa. Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea zawadi zangu, basi tafadhali umpatie mtumishi wako udongo unaoweza kubebwa na nyumbu wawili, kwani toka leo mimi mtumishi wako sitatoa sadaka za kuteketezwa wala tambiko kwa miungu mingine ila tu kwa Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu na anisamehe ninapofuatana na mfalme wangu kwenda kuabudu katika hekalu la Rimoni mungu wa Aramu. Naomba Mwenyezi-Mungu anisamehe!” Elisha akamwambia, “Nenda kwa amani.” Naamani akaenda zake. Alipokuwa bado hajaenda mbali, Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, “Tazama, bwana wangu amemwachilia Naamani Mwaramu aende bila kupokea chochote alicholeta. Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo nitamfuata ili nipate kitu kutoka kwake.” Hapo akaondoka kumfuata Naamani. Naamani alipotazama na kuona mtu anamfuata mbio, akashuka garini mwake akaenda kukutana naye. Basi, akamwuliza, “Je, kuna usalama?” Gehazi akajibu, “Mambo yote ni sawa ila tu bwana wangu amenituma nikuambie kwamba sasa hivi amepokea watu wawili wa kundi la manabii katika nchi ya milima ya Efraimu, naye angependa uwape vipande 3,000 vya fedha na mavazi mawili ya sikukuu.” Naamani akasema, “Tafadhali chukua vipande 6,000 vya fedha.” Akamsihi, kisha akamfungia mafungu mawili na kumpa mavazi mawili ya sikukuu, akawapa watumishi wake wawili na kuwaagiza wafuatane na Gehazi. Walipofika mlimani alipoishi Elisha, Gehazi akachukua mafungu ya fedha kutoka kwa watumishi wa Naamani na kuyapeleka ndani, nyumbani mwake. Kisha akawaruhusu wale watumishi waende zao, nao wakaondoka. Halafu Gehazi akaingia nyumbani kwa Elisha na kuanza kumhudumia. Elisha akamwuliza, “Ulikwenda wapi?” Gehazi akajibu, “Sikuenda mahali popote.” Lakini Elisha akamwambia, “Kwani roho yangu haikuwa pamoja nawe wakati mtu yule alipotoka garini mwake na kuja kukutana nawe? Je, huu ndio wakati wa kupokea fedha na mavazi, mashamba ya mizeituni na mizabibu, kondoo na ng'ombe au watumishi wa kiume na wa kike? Kwa hiyo ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazawa wako milele.” Basi, Gehazi aliondoka akiwa tayari ameshikwa na ukoma, na ngozi yake ilikuwa nyeupe kama theluji. Siku moja, wanafunzi wa manabii walimlalamikia Elisha wakisema, “Mahali hapa tunapokaa ni padogo sana kwetu! Turuhusu twende Yordani tukate miti ili tujijengee mahali patakapotutosha.” Elisha akawajibu, “Nendeni.” Mmoja wao akamwomba akisema, “Tafadhali uwe radhi uende na watumishi wako.” Naye akajibu, “Nitakwenda.” Hivyo akaenda pamoja nao, na walipofika mtoni Yordani wakaanza kukata miti. Mmoja wao alipokuwa anakata miti, shoka lake likachomoka na kuanguka majini; akalia, akisema, “Sasa bwana wangu nitafanya nini? Shoka hili tulikuwa tumeliazima!” Elisha akauliza, “Liliangukia wapi?” Mtu huyo akamwonesha. Elisha akakata kijiti na kukitupa majini na papo hapo shoka likaelea juu ya maji. Elisha akamwamuru alichukue naye akanyosha mkono, akalichukua. Wakati mmoja kulikuwa na hali ya vita kati ya Aramu na Israeli. Basi, mfalme wa Aramu akashauriana na maofisa wake kuhusu mahali watakaposhambulia. Lakini Elisha akampelekea habari mfalme wa Israeli ajihadhari na mahali hapo, kwa kuwa Waaramu walikuwa tayari kupashambulia. Basi, mfalme wa Israeli akapeleka askari wake karibu na mahali alipoambiwa. Elisha aliendelea kumwonya mfalme naye mfalme alijiweka katika hali ya tahadhari. Jambo hilo lilifanyika mara nyingi. Mfalme wa Aramu akafadhaishwa sana na hali hiyo; akawaita maofisa wake, akawauliza, “Niambieni nani kati yenu anayetusaliti kwa mfalme wa Israeli?” Mmoja wao akajibu, “Hakuna anayetusaliti, ee mfalme. Anayehusika ni Elisha, nabii aliyeko huko Israeli. Yeye humwambia mfalme wa Israeli chochote unachosema hata ukiwa katika chumba chako cha kulala.” Mfalme akawaambia, “Nendeni mkapeleleze mjue mahali alipo nami nitawatuma watu wamkamate.” Basi, wakamwarifu kwamba Elisha alikuwa huko Dothani. Kwa hiyo mfalme akapeleka huko jeshi kubwa pamoja na farasi na magari ya kukokotwa. Jeshi hilo likafika huko wakati wa usiku na kuuzingira mji. Mtumishi wa Elisha alipoamka mapema kesho yake na kutoka nje, akaona jeshi pamoja na farasi na magari ya kukokotwa limeuzingira mji. Akarudi ndani akasema, “Ole wetu, ee, Bwana wangu! Sasa tutafanya nini?” Elisha akamjibu, “Usiogope kwa sababu walio pamoja nasi ni wengi kuliko walio pamoja nao.” Kisha Elisha akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, umfumbue macho ili apate kuona!” Basi, Mwenyezi-Mungu akamfumbua macho huyo kijana, akaona farasi na magari ya moto yakiwa kila mahali katika mlima wote, kumzunguka Elisha. Waaramu waliposhambulia, Elisha alimwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Nakuomba uwafanye watu hawa wawe vipofu!” Mwenyezi-Mungu akasikiliza ombi lake na kuwafanya vipofu. Ndipo Elisha akawaendea na kuwaambia, “Mmepotea njia. Huu siyo mji ambao mnautafuta. Nifuateni nami nitawapeleka kwa yule mnayemtafuta.” Naye akawaongoza mpaka Samaria. Mara walipoingia mjini, Elisha akaomba, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, wafumbue macho ili waone.” Mwenyezi-Mungu akasikia ombi lake, akawafumbua macho. Nao wakajikuta wako katikati ya mji wa Samaria. Mfalme wa Israeli alipowaona Waaramu, alimwuliza Elisha, “Je, baba, niwaue?” Elisha akajibu, “La, usiwaue. Kwani hawa unaotaka kuwaua uliwateka kwa upanga wako na mshale wako? Wape chakula na maji, wale na kunywa kisha uwaache warudi kwa bwana wao.” Mfalme wa Israeli akawafanyia karamu kubwa; walipomaliza kula na kunywa, akawarudisha kwa bwana wao. Toka wakati huo, Waaramu hawakuishambulia tena nchi ya Israeli. Baadaye, mfalme Ben-hadadi wa Aramu akakusanya jeshi lake lote akatoka na kuuzingira mji wa Samaria. Matokeo yake ilikuwa njaa kali katika mji wa Samaria. Kichwa cha punda kiligharimu vipande themanini vya fedha, na gramu 100 za mavi ya njiwa ziligharimu vipande vitano vya fedha. Siku moja mfalme wa Israeli alipokuwa anatembea juu ya ukuta wa mji, alisikia mwanamke mmoja akimwita, “Nisaidie, ee bwana wangu mfalme!” Mfalme akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asipokusaidia, mimi nitakupa msaada kutoka wapi; kutoka katika kiwanja cha kupuria au kutoka katika shinikizo? Shida yako ni nini?” Akamjibu, “Juzi mwanamke huyu alinishauri tumle mwanangu na kesho yake tumle wake. Tukampika mwanangu, tukamla. Kesho yake nikamwambia tumle mwanawe, lakini alikuwa amemficha!” Mara mfalme aliposikia maneno ya mwanamke huyo alirarua nguo zake kwa huzuni, na watu waliokuwa karibu na ukuta waliona kwamba alikuwa amevaa vazi la gunia ndani yake. Naye akasema, “Mungu aniue, Elisha mwana wa Shafati asipokatwa kichwa leo!” Ndipo akatuma mjumbe kwenda kumleta Elisha. Wakati huohuo Elisha alikuwa nyumbani pamoja na wazee waliomtembelea. Kabla ya mjumbe wa mfalme kufika, Elisha akawaambia wazee, “Yule muuaji amemtuma mtu kuja kunikata kichwa! Atakapofika hapa, fungeni mlango, wala msimruhusu aingie. Pia bwana wake anamfuata nyuma.” Kabla hata hajamaliza kusema, mfalme akafika, akasema, “Msiba huu umetoka kwa Mwenyezi-Mungu! Kwa nini niendelee kumngojea tena?” Elisha akamjibu, “Sikiliza neno la Mwenyezi-Mungu: Kesho wakati kama huu, humu Samaria kilo tatu za unga bora wa ngano zitagharimu fedha shekeli moja ya fedha, na kilo sita za shayiri kadhalika zitagharimu fedha shekeli moja.” Kapteni mwaminifu wa mfalme akamwambia Elisha, “Kama Mwenyezi-Mungu mwenyewe angefanya madirisha mbinguni, je, jambo hilo litawezekana!” Elisha akamjibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula.” Kulikuwa na watu wanne wenye ugonjwa wa ukoma waliokuwa nje ya milango ya mji wa Samaria ambao walisemezana, wao kwa wao, “Mbona tunakaa hapa tukifa njaa? Hakuna maana ya kuingia mjini kwa sababu huko tutakufa. Kwa hiyo hebu twende kwenye kambi ya Waaramu; inawezekana wakatuua, au wasituue.” Hivyo, giza lilipoanza kuingia, wakaenda kwenye kambi ya Waaramu, lakini walipofika huko, hapakuwa na mtu. Maana Mwenyezi-Mungu alilifanya jeshi la Waaramu lisikie sauti kama ya jeshi kubwa lililokuwa na magari na farasi. Waaramu wakadhani kuwa mfalme wa Israeli amekodisha majeshi ya Wahiti na Wamisri kuja kuwashambulia. Basi, katika usiku huo, Waaramu walikimbia wote ili kuyaokoa maisha yao wakiacha mahema yao, farasi na punda wao, na hata kambi yao jinsi ilivyokuwa. Wakoma wale wanne walipofika pembeni mwa kambi, waliingia ndani ya hema moja, wakala na kunywa vile walivyopata humo, wakachukua fedha, dhahabu na nguo, wakaenda kuzificha. Wakaingia katika hema nyingine na kufanya vivyo hivyo. Lakini wakaambiana, “Tunalofanya si sawa! Hii ni habari njema tuliyo nayo leo, na ikiwa tutangoja mpaka asubuhi, bila shaka tutaadhibiwa. Twende mara moja tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme!” Hivyo, wakaondoka katika kambi ya Waaramu na kuwaita mabawabu wa mji na kuwaambia: “Tulikwenda katika kambi ya Waaramu na hatukuweza kumwona wala kumsikia mtu yeyote. Farasi na punda wangali wamefungwa, na mahema yako kama walivyoyaacha.” Walinda malango wakaeneza habari hizi mpaka zikafika nyumbani kwa mfalme. Ingawa kulikuwa bado giza, mfalme aliamka na kuwaambia maofisa wake, “Mimi najua mpango wa Waaramu! Wanajua tuna njaa mjini, sasa wameacha kambi yao kwenda kujificha ili tutakapokwenda kutafuta chakula, watukamate sote hai na kuuteka mji.” Mmoja kati ya maofisa wake akasema, “Watu wengi tayari wameangamia kama vile wale ambao wamekwisha fariki. Tafadhali utume watu wachache na farasi watano wa wale waliobaki ili waende kuona kumetokea nini.” Wakachagua watu na kuwapa magari mawili. Mfalme akawatuma kuwafuata Waaramu, akisema, “Nendeni mkaone.” Watu hao wakaenda mpaka Yordani na njiani waliona nguo na vifaa vingine Waaramu walivyoacha walipokuwa wanakimbia. Wakarudi na kumpasha mfalme habari. Watu wa Samaria wakatoka na kuteka nyara kambi ya Waaramu. Kama vile Mwenyezi-Mungu alivyosema: Kilo tano za unga safi wa ngano au kilo kumi za shayiri ziliuzwa kwa kipande kimoja cha fedha. Naye mfalme alikuwa amemweka ofisa mlinzi wake kulinda lango la mji. Ofisa huyo alikanyagwa papo hapo langoni na kuuawa na watu, kama vile Elisha mtu wa Mungu alivyotabiri wakati mfalme alipokwenda kumwona. Elisha alikuwa amemwambia mfalme kwamba wakati kama huo siku iliyofuata, kilo tano za unga mzuri wa ngano au kilo kumi za shayiri zingeuzwa kwa kipande kimoja cha fedha; lakini hapo awali kapteni alikuwa amembishia Elisha, akisema, “Kama Mwenyezi-Mungu mwenyewe angefanya madirisha mbinguni, je, jambo hili lingewezekana?” Naye Elisha alikuwa amemjibu, “Utaona yakitendeka, lakini chakula chenyewe hutakila.” Na hivyo ndivyo ilivyotokea — kapteni akafa kwa kukanyagwa na watu kwenye lango la mji. Elisha alikuwa amemwambia mwanamke aliyeishi Shunemu ambaye alikuwa amemfufua mwanawe, “Ondoka, na jamaa yako, uhamie ugenini kwa sababu Mwenyezi-Mungu ameleta njaa itakayokuwamo nchini kwa muda wa miaka saba.” Akamshauri ahame aende mahali pengine. Huyo mwanamke akaondoka akafanya kama mtu wa Mungu alivyosema akaenda pamoja na jamaa yake na kukaa kama mgeni katika nchi ya Filistia kwa miaka saba. Miaka saba ilipokwisha, alitoka Filistia akarudi Israeli na kwenda kwa mfalme kuomba arudishiwe nyumba yake na shamba lake. Akamkuta mfalme anaongea na Gehazi, akisema, “Tafadhali nieleze miujiza ambayo hutendwa na Elisha.” Gehazi alipokuwa anamweleza mfalme jinsi Elisha alivyofufua mtu aliyekufa, mwanamke huyo alitoa ombi lake kwa mfalme. Gehazi akasema, “Ee mfalme; huyu ndiye mwanamke ambaye Elisha alimfufua mwanawe!” Mfalme alipomwuliza mwanamke huyo, yeye alimweleza. Mfalme akamwita ofisa wake na kumwamuru amrudishie mwanamke huyo mali yake yote, pamoja na mapato yote ya mashamba yake katika muda huo wote wa miaka saba. Baadaye Elisha alikwenda Damasko. Wakati huo mfalme Ben-hadadi alikuwa mgonjwa na alipoambiwa kwamba Elisha alikuwa Damasko, alimwambia ofisa wake Hazaeli, “Mpelekee mtu wa Mungu zawadi umwambie atafute shauri kwa Mwenyezi-Mungu kama nitapona au la.” Hazaeli akapakia zawadi za kila aina ya mazao ya Damasko kiasi cha mizigo ya ngamia arubaini na kumpelekea Elisha. Alipofika kwa Elisha alimwambia, “Mtumishi wako, Ben-hadadi, mfalme wa Aramu amenituma kwako; yeye anauliza, ‘Nitapona ugonjwa huu?’” Basi Elisha akamjibu, “Atapona; lakini Mwenyezi-Mungu amenionesha kwamba atakufa.” Ndipo Elisha akamkazia macho akiwa na hofu hata Hazaeli akashikwa na wasiwasi. Ghafla, Elisha mtu wa Mungu, akaanza kulia. Hazaeli akamwuliza, “Bwana wangu, mbona unalia?” Elisha akamjibu, “Kwa sababu ninajua maovu ambayo utawatendea watu wa Israeli. Utateketeza ngome zao kwa moto, na kuwaua vijana wao, utawapondaponda watoto wao na kuwararua wanawake waja wazito.” Hazaeli akauliza, “Lakini mimi mtumishi wako ni kitu kweli? Mimi niliye mbwa tu nitawezaje kutenda mambo hayo makubwa?” Elisha akamjibu, “Mwenyezi-Mungu amenionesha kwamba utakuwa mfalme wa Aramu.” Ndipo Hazaeli alipotoka kwa Elisha, akarudi kwa bwana wake. Mfalme Ben-hadadi akamwuliza, “Elisha alikuambia nini?” Hazaeli akamjibu, “Aliniambia ya kwamba hakika utapona.” Lakini kesho yake Hazaeli akachukua blanketi akalilowesha majini, kisha akamfunika nalo usoni mpaka akafa. Hazaeli akatawala Aramu mahali pake. Mnamo mwaka wa tano wa utawala wa Yoramu mwana wa Ahabu, mfalme wa Israeli, Yehoramu mwana wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alianza kutawala akiwa na umri wa miaka thelathini na miwili. Alitawala huko Yerusalemu miaka minane. Alizifuata njia mbaya za wafalme wengine wa Israeli, kama jamaa ya Ahabu ilivyofanya, kwa sababu mkewe alikuwa binti Ahabu. Akatenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini Mwenyezi-Mungu hakutaka kuangamiza Yuda, kwa sababu ya Daudi mtumishi wake, kwani aliahidi kwamba wazawa wake wataendelea kutawala milele. Wakati wa enzi ya Yehoramu, watu wa Edomu waliasi utawala wa Yuda, wakamtawaza mfalme wao. Kwa hiyo Yoramu aliondoka na magari yake yote kwenda Zairi. Wakati wa usiku alitoka na makamanda wake wa magari akawashambulia Waedomu waliokuwa wamemzunguka; lakini jeshi lake lilikimbia nyumbani. Hivyo watu wa Edomu wakauasi utawala wa Yuda mpaka sasa. Wakati huohuo, wakazi wa Libna nao wakaasi. Matendo mengine yote ya mfalme Yehoramu yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Yehoramu akafa na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi, naye Ahazi, mwanawe Yehoramu, akatawala mahali pake. Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda, alianza kutawala. Ahazia alianza kutawala akiwa na umri wa miaka ishirini na miwili, akatawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa mfalme Omri mfalme wa Israeli. Kwa sababu Ahazia alikuwa mkwe wa jamaa ya Ahabu, naye alifuata mwenendo wa jamaa hiyo ya Ahabu, alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama vile jamaa ya Ahabu walivyofanya. Mfalme Ahazia akaenda na Yoramu mwana wa Ahabu kupigana vita dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-gileadi mahali Waaramu walipomjeruhi Yoramu. Kisha mfalme Yoramu akarudi mjini Yezreeli ili apate kutibiwa majeraha aliyoyapata huko Rama, alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alimwendea Yoramu mwana wa Ahabu huko Yezreeli, kwa sababu alikuwa mgonjwa. Wakati huohuo nabii Elisha alimwita mmoja wa wanafunzi wa manabii, akamwambia, “Jitayarishe kwenda Ramothi katika Gileadi. Chukua chupa hii ya mafuta na utakapofika huko, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati na mjukuu wa Nimshi. Mchukue kando chumbani mbali na wenzake, kisha chukua chupa hii ya mafuta, ummiminie kichwani na kumwambia, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimekupaka mafuta kuwa mfalme wa Israeli.’ Kisha fungua mlango na kuondoka upesi utakavyoweza.” Basi, Nabii huyo kijana akaenda Ramothi Gileadi. Alipofika aliwakuta makamanda wa jeshi mkutanoni. Akasema “Nina ujumbe wako, kamanda.” Yehu akamwuliza, “Ni nani kati yetu unayemwambia?” Akamjibu, “Wewe, kamanda.” Ndipo wote wawili wakaingia chumba cha ndani na huko nabii akamtia Yehu mafuta kichwani na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema, ‘Nakupaka mafuta uwe mfalme juu ya watu wangu Israeli. Nawe utaipiga jamaa ya bwana wako Ahabu ili nimlipize kisasi Yezebeli damu ya watumishi wangu manabii na ya watumishi wangu wote. Utafanya hivyo kwa sababu jamaa yote ya Ahabu itaangamia; pia nitamkatilia mbali kila mwanamume wa jamaa ya Ahabu awe mtumwa au mtu huru. Jamaa yake itakuwa kama jamaa ya Yeroboamu mwana wa Nebati na ya Baasha mwana wa Ahiya. Yezebeli hatazikwa na mtu, maiti yake italiwa na mbwa katika nchi ya Yezreeli.’” Baada ya kusema hayo, nabii akaondoka chumbani na kukimbia. Yehu aliporudi kwa wenzake, mmoja wao alimwuliza, “Kuna shida yoyote? Mwendawazimu huyu alitaka nini kwako?” Yehu akawajibu, “Mnajua alichotaka.” Nao wakamwambia, “Hiyo si kweli! Tuambie alilosema!” Akawaambia, “Aliniambia kwamba Mwenyezi-Mungu amesema, ‘Nimekutawaza kuwa mfalme wa Israeli.’” Mara moja makamanda wenzake wakavua mavazi yao, wakayarundika pamoja kwenye ngazi ili asimame juu yake, wakapiga tarumbeta na kupaza sauti, “Yehu ni mfalme!” Yehu mwana wa Yehoshafati, ambaye pia alikuwa mjukuu wa Nimshi, alikula njama dhidi ya Yoramu. Yoramu na watu wote wa Israeli walikuwa Ramoth-gileadi kulinda zamu dhidi ya mfalme Hazaeli wa Aramu. Lakini mfalme Yoramu alikuwa amerudi Yezreeli ili apone majeraha aliyopata wakati wa kupigana vitani na mfalme Hazaeli wa Aramu. Yehu aliwaambia maofisa wenzake; “Ikiwa mtakubaliana nami, mtu yeyote asitoke Ramothi kwenda Yezreeli kupeleka habari hizi.” Ndipo akapanda gari lake na kuelekea Yezreeli. Yoramu alikuwa bado hajapona, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa amemtembelea. Mlinzi aliyekuwa kwa zamu juu ya mnara wa Yezreeli akasema, “Naona watu wakija na gari!” Yoramu akajibu, “Chagua mpandafarasi mmoja, umtume ili akutane nao, awaulize ‘Kuna amani?’” Basi, mjumbe huyo alipokwenda alikutana na Yehu na kumwambia, “Mfalme anauliza: Kuna amani?” Yehu akajibu, “Kwa nini unauliza kuhusu amani? Wewe geuka ufuatane nami!” Mlinzi juu ya mnara akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini harudi.” Ndipo mjumbe wa pili akatumwa, ambaye pia alimwuliza Yehu swali hilohilo. Yehu akamwambia vivyo hivyo, “Kwa nini unauliza kuhusu amani? Wewe geuka ufuatane nami!” Kwa mara nyingine tena mlinzi akasema “Mjumbe amewafikia lakini harudi.” Halafu akaongeza, “Uendeshaji wa gari ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi; kwa sababu yeye huendesha kwa kasi.” Basi, Yoramu mfalme wa Israeli akaamuru akisema, “Tayarisha gari.” Nao walitayarisha gari lake. Kisha Yoramu mfalme wa Israeli na Ahazia mfalme wa Yuda waliondoka kila mmoja akipanda gari lake, wakaenda kukutana na Yehu. Walimkuta katika uwanja wa Nabothi Myezreeli. Ikawa Yoramu, alipomwona Yehu, alimwuliza, “Je, kuna amani, Yehu?” Yehu akamjibu, “Amani gani, wakati makahaba na wachawi wa Yezebeli ni wengi?” Yoramu aligeuza gari lake na kuondoka, huku akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini Ahazia!” Yehu akatwaa upinde wake na kutupa mshale ambao ulipenya mabega ya Yoramu na kuchoma moyo wake, naye akafa papo hapo garini mwake. Yehu akamwambia msaidizi wake Bidkari, “Chukua hiyo maiti yake uitupe katika shamba hilo la Nabothi Myezreeli. Kwa maana, kumbuka wewe na mimi tulipokuwa tumepanda farasi wetu nyuma ya baba yake Ahabu, jinsi Mwenyezi-Mungu alivyonena maneno haya dhidi yake. Mwenyezi-Mungu alisema, ‘Kwa ile damu ya Nabothi na kwa damu ya wanawe niliyoona jana naapa kwamba nitakulipiza kisasi katika shamba hilo.’ Kwa hiyo, chukua maiti ya Yoramu uitupe katika shamba la Nabothi kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.” Ahazia mfalme wa Yuda alipoona yaliyotukia alikimbia akielekea Nyumba ya Bustani, huku akifuatwa na Yehu. Yehu akawaamuru watu wake, “Muueni naye pia!” Nao wakampiga mshale akiwa garini kwenye njia ya kupanda Guri karibu na mji wa Ibleamu. Halafu alikimbilia Megido na kufia huko. Maofisa wake wakaichukua maiti yake ndani ya gari lake na kuipeleka Yerusalemu; na huko akazikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi. Ahazia alianza kutawala juu ya Yuda katika mwaka wa kumi na moja wa enzi ya Yoramu mwana wa Ahabu. Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli alikuwa amekwisha pata habari za mambo yaliyotokea. Alijipaka rangi machoni na kupanga nywele zake, ndipo akaenda dirishani na kuangalia chini. Yehu alipokuwa akiingia langoni Yezebeli alisema, “Unakuja kwa amani, ewe Zimri! Wewe unayewaua mabwana zako?” Yehu akaangalia juu na kusema “Ni nani aliye upande wangu?” Maofisa wawili au watatu wakatokeza vichwa vyao kumwangalia kutoka dirishani, naye Yehu akawaambia, “Mtupe chini!” Wakamtupa chini na damu yake ikatapakaa juu ya ukuta na kwenye farasi. Yehu akapitisha farasi na gari lake juu ya maiti yake na kuingia katika jumba la kifalme, na huko akala na kunywa. Halafu akaamuru: “Mzikeni mwanamke huyo aliyelaaniwa; kwa kuwa ni binti mfalme.” Ndipo walipokwenda kumzika; lakini hawakuona chochote isipokuwa fuvu la kichwa, mifupa ya mikono na miguu. Kisha walirudi na kumpasha Yehu habari hizi, naye akasema, “Hivi ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyotabiri kupitia kwa mtumishi wake Elia Mtishbi akisema, ‘Mbwa wataula mwili wa Yezebeli katika nchi ya Yezreeli. Maiti yake Yezebeli itakuwa kama mavi shambani katika nchi ya Yezreeli, hivyo kwamba hakuna atakayeweza kumtambua.’” Katika mji wa Samaria kulikuwa na wana sabini wa Ahabu. Yehu akaandika barua na kuzituma kwa watawala wa mji, kwa viongozi na kwa walinzi wa wana wa Ahabu. Barua yenyewe ilisema hivi: “Kwa kuwa mnao miongoni mwenu wana wa mfalme, kadhalika mnao farasi na magari, silaha na miji ya ngome, mchagueni na kumtawaza mwenye uwezo zaidi kati ya wana wa mfalme; halafu mpige vita kwa ajili ya ukoo wa mfalme.” Watawala wa Samaria waliogopa sana na kusema, “Tunawezaje kumpiga Yehu hali mfalme Yoramu na mfalme Ahazia hawakuweza?” Kwa hiyo ofisa mkuu wa nyumba ya mfalme na ofisa mkuu wa mji, wakishirikiana na viongozi wengine na walinzi, wakampelekea Yehu ujumbe huu: “Sisi tu watumwa wako, na tuko tayari kufanya lolote unalosema. Lakini hatutamtawaza mtu yeyote kuwa mfalme; fanya unavyoona vyema.” Yehu akawaandikia barua nyingine akiwaambia: “Ikiwa kweli mko tayari kufuata maagizo yangu, leteni hapa Yezreeli vichwa vya wana wa bwana wenu; nivipate kesho wakati kama huu.” Wana sabini wa mfalme Ahabu waliishi kwa viongozi wa Samaria, ambao walikuwa walezi wao. Basi, barua ilipowafikia waliwachukua hao wana wa mfalme na kuwakata wote sabini. Waliweka vichwa vyao vikapuni na kumpelekea Yehu huko Yezreeli. Kisha mtumishi mmoja akamwendea na kusema, “Vichwa vya wana wa mfalme vimekwisha letwa.” Ndipo akaamuru, “Viwekwe chini katika mafungu mawili kwenye lango la mji; halafu viache vikae huko mpaka asubuhi.” Asubuhi yake akatoka, akasimama na kuwaambia watu wote, “Nyinyi ni waadilifu, angalia mimi nilikula njama dhidi ya bwana wangu na kumuua. Lakini ni nani aliyewaua hawa wote? Jueni ya kwamba maneno yote aliyosema Mwenyezi-Mungu kuhusu jamaa ya Ahabu yametimia. Mwenyezi-Mungu ameyafanya hayo aliyosema kwa njia ya mtumishi wake Elia.” Ndipo Yehu akaua jamaa yote ya Ahabu iliyokuwa inakaa Yezreeli, pamoja na maofisa wake na marafiki na makuhani wake; hakumwacha mtu yeyote. Baadaye Yehu aliondoka Yezreeli, akaelekea Samaria. Akiwa njiani mahali panapoitwa “Kambi ya Wachungaji,” alikutana na jamaa za marehemu Ahazia mfalme wa Yuda akawauliza, “Nyinyi ni kina nani?” Wakamjibu, “Sisi ni jamaa za Ahazia. Tumeteremka huku kuwatembelea wana wa mfalme na wana wa malkia.” Kisha akasema, “Wakamateni wakiwa hai.” Wakawakamata watu arubaini na wawili, wakawaulia karibu na kisima cha “Kambi ya Wachungaji.” Hakuna aliyebaki hata mmoja. Yehu akatoka tena na alipofika njiani akakutana na Yehonadabu mwana wa Rekabu; Yehu akamsalimu, kisha akamwambia “Wewe una mawazo sawa na yangu? Je, utajiunga nami na kunisaidia?” Yehonadabu akamjibu, “Naam, nitajiunga nawe:” Yehu akasema, “Basi, nipe mkono wako.” Wakashikana mikono na Yehu akampandisha garini mwake. Akamwambia, “Fuatana nami ili ujionee jinsi nilivyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu.” Basi, wakasafiri pamoja garini mwake. Walipofika Samaria, Yehu aliua jamaa yote ya Ahabu bila kumwacha hata mmoja wao. Ikawa sawa kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Elia itakavyokuwa. Yehu akawakusanya watu wa Samaria na kuwaambia, “Mfalme Ahabu alimtumikia Baali kidogo tu, lakini mimi nitamtumikia zaidi. Waite manabii wote wa Baali, wafuasi wake wote na makuhani. Ni sharti kila mmoja afike, kwani nataka kumtolea Baali tambiko kubwa, na yeyote atakayekosa kufika atauawa.” Hiyo ilikuwa ni njama ya Yehu ili apate kuwaua wafuasi wa Baali. Yehu akaamuru: “Alika mkutano mkubwa wa ibada ya Baali!” Tangazo likatolewa, na Yehu akapeleka habari katika nchi yote ya Israeli ili wafuasi wote wa Baali wahudhurie kila mmoja. Wakaja wote na kujaa katika hekalu la Baali kutoka pembe moja mpaka nyingine. Ndipo Yehu akamwagiza aliyesimamia mavazi matakatifu akisema, “Toa mavazi hayo na kuwapa watu waliohudhuria ibada.” Msimamizi akatoa mavazi hayo, akawapa. Halafu Yehu akaingia katika hekalu la Baali akifuatana na Yehonadabu na kuwaambia waliokuwa hekaluni, “Hakikisheni kwamba waliomo hekaluni ni wale wamwabuduo Baali tu, na kwamba hakuna mtu yeyote anayemwabudu Mwenyezi-Mungu. Kisha akaingia pamoja na Yehonadabu kumtolea Baali matambiko na tambiko za kuteketezwa. Yehu alikuwa ameweka watu themanini nje ya hekalu na kuwapa maagizo haya: ‘Waueni watu hawa wote. Yeyote atakayemwacha hata mmoja wao atoroke atalipa kwa maisha yake!’” Mara Yehu alipomaliza kutoa tambiko ya kuteketezwa, aliwaambia walinzi na maofisa, “Ingieni mkawaue wote. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakaingia na panga zao tayari na kuwaua wote, kisha wakatoa maiti zao nje. Ndipo wakaingia chumba cha ndani cha hekalu, na kutoa nguzo takatifu na kuiteketeza kwa moto. Wakaharibu nguzo pamoja na hekalu; wakaligeuza hekalu kuwa choo; na hivyo ndivyo ilivyo mpaka hivi leo. Hivyo ndivyo Yehu alivyofuta ibada za Baali katika Israeli. Lakini alifuata dhambi ya Yeroboamu mwana wa Nebati ya kuwaongoza Waisraeli watende dhambi. Aliweka sanamu za ndama wa dhahabu huko Betheli na Dani. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yehu, “Umewatendea wazawa wa Ahabu yale yote niliyotaka uwatendee. Kwa hiyo nimekuahidi kuwa wazawa wako hadi kizazi cha nne watatawala Israeli.” Lakini Yehu hakutii sheria za Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote. Badala yake, alifuata mfano wa Yeroboamu aliyewapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Wakati huo Mwenyezi-Mungu alianza kupunguza eneo la nchi ya Israeli. Mfalme Hazaeli wa Aramu akashinda nchi yote ya Israeli, kutoka upande wa mashariki ya mto Yordani, na nchi za Gileadi, Gadi, Reubeni na Manase na kutoka Aroeri ulioko kwenye bonde la Arnoni, kwenye nchi za Gileadi na Bashani. Matendo mengine yote ya Yehu na vitendo vyake vya ushujaa yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Akafariki na kuzikwa Samaria. Mwanae Yehoahazi akatawala mahali pake. Yehu alitawala Israeli akiwa Samaria kwa miaka ishirini na minane. Mara Athalia, mamake mfalme Ahazia, alipoona kuwa mwanawe ameuawa, alitoka, akaangamiza jamii yote ya kifalme. Lakini Yehosheba binti ya mfalme Yoramu, dada yake Ahazia, alimchukua kwa siri Yoashi mwana wa Ahazia, kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Alimficha yeye pamoja na yaya wake katika chumba cha kulala. Hivyo walimficha ili Athalia asimwone na kumwua. Yoashi alikaa naye kwa muda wa miaka sita akiwa amefichwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakati Athalia alipokuwa akitawala nchi. Lakini katika mwaka wa saba Yehoyada alituma ujumbe na kuwakusanya makapteni wa Wakari na walinzi; akaamuru wamjie katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akafanya nao mapatano na kuwaapisha humo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu akawaonesha Yoashi mwana wa mfalme Ahazia. Kisha akatoa amri: “Mtafanya hivi: Mtakapokuja kushika zamu siku ya Sabato, theluthi moja italinda ikulu; theluthi nyingine ikiwa kwenye lango la Suri na theluthi nyingine ikiwa kwenye lango nyuma ya walinzi. Hivyo ndivyo mtakavyolinda ikulu ili isivunjwe. Yale makundi mawili ambayo humaliza zamu yao siku ya Sabato yatashika zamu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kumlinda mfalme. Mtamzunguka mfalme, kila mtu na silaha yake mkononi na mtu yeyote atakayethubutu kuwakaribia lazima auawe. Lazima mkae na mfalme, awe anatoka au anakaa.” Makapteni walitii amri zote alizotoa kuhani Yehoyada. Kila ofisa akawachukua watu wake wote, wale waliokuwa wamemaliza zamu na wale waliokuwa wanaingia kushika zamu siku ya Sabato, basi wakamwendea kuhani Yehoyada. Kisha kuhani akawapa makapteni mikuki na ngao zilizokuwa mali ya mfalme Daudi, na ambazo zilikuwa zimewekwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nao walinzi walisimama kuanzia upande wa kusini wa nyumba mpaka upande wa kaskazini wa nyumba na kuzunguka madhabahu na nyumba ili kumzunguka mfalme; kila mtu akiwa ameshika mkuki wake mkononi. Halafu akamtoa nje mwana wa mfalme, akamvika taji kichwani, na kumpa ule ushuhuda; wakamtawaza na kumpaka mafuta; wakapiga makofi na kusema, “Aishi mfalme!” Naye Athalia aliposikia sauti za walinzi pamoja na za watu wengine, aliwaendea hao watu waliokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Alipochungulia akamwona mfalme mpya amesimama karibu na nguzo kwenye lango la hekalu, kama ilivyokuwa desturi, huku makapteni na wapiga tarumbeta wakiwa kando ya mfalme; na wakazi wote wakishangilia na kupiga tarumbeta; ndipo aliporarua nguo zake na kusema kwa sauti kubwa, “Uhaini! Uhaini!” Kisha kuhani Yehoyada akaamuru makapteni wa jeshi akisema; “Mtoeni nje katikati ya askari, na ueni mtu yeyote atakayemfuata.” Kwa sababu kuhani alisema, “Asiuawe katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Basi, wakamkamata, wakampeleka na kumpitisha kwenye Lango la Farasi kuelekea ikulu, naye akauawa huko. Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Mwenyezi-Mungu na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa Mwenyezi-Mungu; kadhalika alifanya agano kati ya mfalme na watu. Halafu wakazi wote wakaenda kwenye nyumba ya Baali na kuibomoa, wakavunja madhabahu pamoja na sanamu zake, hata wakamuua Matani, kuhani wa Baali mbele ya madhabahu. Kuhani Yehoyada akaweka walinzi kulinda nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Aliwachukua makapteni, Wakari na wakazi wote; nao wakamsindikiza mfalme kutoka nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakapitia katika lango la walinzi mpaka ikulu. Naye akakikalia kiti cha enzi. Kwa hiyo, wakazi wote walijawa furaha; na mji wote ulikuwa mtulivu, baada ya Athalia kuuawa kwa upanga katika ikulu. Yoashi alianza kutawala Yuda akiwa na umri wa miaka saba. Katika mwaka wa saba wa enzi ya mfalme Yehu wa Israeli Yoashi alianza kutawala Yuda huko Yerusalemu, naye akatawala kwa muda wa miaka arubaini huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Sibia, kutoka Beer-sheba. Wakati wa maisha yake yote alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu kuhani Yehoyada alikuwa akimfundisha. Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia miungu hapakuharibiwa, na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani huko. Yoashi akaita makuhani na kuwaamuru, akisema, “Fedha yote inayoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ikiwa imetokana na uuzaji wa vitu vitakatifu, fedha ya kila mtu kadiri alivyoandikiwa, na fedha ambayo mtu huvutwa kuitoa kwa hiari katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, makuhani wazipokee kutoka kwa kila mtu; nao warekebishe nyumba popote panapohitajika marekebisho.” Lakini hata baada ya miaka ishirini na mitatu ya mfalme Yoashi makuhani walikuwa bado hawajafanya marekebisho yoyote ya nyumba. Kwa hiyo mfalme Yoashi alimwita kuhani Yehoyada na makuhani wengine na kuwauliza, “Mbona hamrekebishi nyumba? Basi, msichukue fedha kutoka kwa watu mnaowatumikia, bali mtazileta, ili nyumba irekebishwe.” Makuhani wakakubali wasipokee fedha tena kutoka kwa watu na pia wakaahidi kutofanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Yehoyada akachukua sanduku na kutoboa tundu kwenye kifuniko chake, kisha akaliweka kwenye madhabahu upande wa kulia, mtu anapoingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani waliokuwa katika zamu langoni waliweka fedha zote zilizoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kila walipoona kuwa mna fedha nyingi sandukuni, katibu wa mfalme na kuhani mkuu waliingia na kuhesabu na kuzifunga katika vifurushi fedha zote zilizopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kisha baada ya kuzipima waliwapa wafanyakazi waliosimamia nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nao wakawalipa maseremala na wajenzi, waliorekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu; pia waashi na wakata-mawe, zikatumiwa kununulia mbao na mawe yaliyochongwa ili kufanyia marekebisho nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kutimiza mahitaji mengine yote ya marekebisho ya nyumba. Lakini pesa hizo hazikutumiwa kwa kulipia utengenezaji wa mabirika ya fedha, mikasi ya kukatia tambi za mishumaa, mabakuli, tarumbeta, wala kwa vyombo vingine vyovyote vya dhahabu au vya fedha. Zote zilitumiwa kwa kuwalipa wafanyakazi waliozitumia kufanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Wafanyakazi waliosimamia kazi hii walikuwa waaminifu kabisa, kwa hiyo hapakuwa na haja ya kuwataka watoe hesabu ya matumizi ya fedha hizo. Fedha zilizotolewa kuwa sadaka za hatia na sadaka za kuondoa dhambi hazikuingizwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu; hizo zilikuwa ni mali ya makuhani. Wakati huo Hazaeli mfalme wa Aramu akaushambulia mji wa Gathi na kuuteka. Lakini Hazaeli alipoelekea Yerusalemu ili aushambulie, Yoashi mfalme wa Yuda alichukua sadaka zote zilizowekwa wakfu na babu zake wafalme wa Yuda: Yehoshafati, Yehoramu na Ahazia, na kuongeza zile zake, pamoja na dhahabu yote iliyokuwa katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika ikulu, akazituma kwa Hazaeli mfalme wa Aramu. Naye Hazaeli akatoka Yerusalemu. Matendo mengine yote ya mfalme Yoashi yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Maofisa wake walikula njama dhidi yake, wakamuulia katika nyumba ya Milo kwenye barabara inayoelekea Sila. Waliomuua ni Yozakari mwana wa Shimeathi na Yehozabadi mwana wa Shomeri watumishi wake. Halafu walimzika katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi; naye Amazia, mwanawe, akatawala mahali pake. Katika mwaka wa ishirini na tatu wa enzi ya mfalme Yoashi wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli, akaendelea kutawala huko Samaria muda wa miaka kumi na saba. Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati aliyewakosesha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Yehoahazi hakuacha matendo hayo mabaya. Mwenyezi-Mungu alikasirika, akawafanya watu wa Israeli washindwe vitani mara kwa mara na mfalme Hazaeli wa Aramu na mwanawe Ben-hadadi. Yehoahazi akamsihi Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu alipoona jinsi mfalme wa Aramu alivyowadhulumu watu wa Israeli alisikia maombi yake. (Mwenyezi-Mungu akawapa watu wa Israeli kiongozi ambaye aliwakomboa kutoka kwa Washamu, ndipo wakakaa kwa amani kama vile walivyokuwa hapo awali. Hata hivyo hawakuacha kutenda dhambi ambazo mfalme Yeroboamu aliwakosesha watu wa Israeli; lakini waliendelea na dhambi zao na sanamu ya mungu wa kike Ashera ilihifadhiwa huko Samaria.) Yehoahazi hakuwa na majeshi, ila tu wapandafarasi hamsini, magari kumi na askari wa miguu 10,000. Hii ilikuwa ni kwa sababu mfalme wa Aramu alikuwa ameyaangamiza majeshi ya Israeli na kuyakanyaga chini kama mavumbi. Matendo mengine yote ya Yehoahazi na ushujaa wake yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Yehoahazi alifariki na kuzikwa huko Samaria, naye mwanawe Yehoashi akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa thelathini na saba wa enzi ya mfalme Yoashi wa Yuda, Yehoashi mwanawe Yehoahazi, alianza kutawala Israeli huko Samaria, na enzi yake ikaendelea kwa miaka kumi na sita. Yehoashi pia alitenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu na kufuata mfano wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati ambaye aliwapotosha watu wa Israeli. Matendo mengine yote ya Yehoashi, ushujaa wake na vita alivyopigana na mfalme Amazia wa Yuda, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Yehoashi alifariki na kuzikwa katika makaburi ya kifalme huko Samaria, naye mwanawe Yeroboamu wa pili akatawala mahali pake. Nabii Elisha aliugua ugonjwa mbaya sana. Alipokuwa karibu kufa, mfalme Yehoashi wa Israeli alimtembelea. Alipomfikia Elisha, alilia, akisema, “Baba yangu, baba yangu! Magari ya Israeli na wapandafarasi wake!” Elisha akamwamuru, “Hebu lete upinde na mishale!” Yehoashi akavileta. Elisha akamwambia ajitayarishe kupiga mishale. Mfalme akajitayarisha na Elisha akaiweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Mfalme alifuata maagizo ya nabii na kufungua dirisha ambalo lilielekea Aramu. Elisha akatoa amri “Tupa mshale!” Mara tu mfalme alipotupa mshale, nabii akasema, “Wewe ndio mshale wa Mwenyezi-Mungu, ambao kwao atapata ushindi juu ya Waaramu. Utapigana na Waaramu huko Afeka mpaka uwashinde.” Ndipo Elisha akamwambia mfalme achukue mishale mingine na kuipiga chini. Mfalme akapiga mishale chini mara tatu, kisha akaacha. Elisha alikasirika sana, akamwambia mfalme, “Mbona hukupiga mara tano au sita? Hivyo ungewaangamiza Waaramu kabisa. Lakini sasa utawashinda mara tatu tu.” Elisha alifariki, akazikwa. Kila mwaka, makundi ya Wamoabu yalikuja kuishambulia nchi ya watu wa Israeli. Wakati mmoja, wakati wa mazishi, watu waliona kundi mojawapo la watu waliobeba maiti wakamtupa yule maiti kaburini mwa Elisha na kukimbia. Mara maiti huyo alipogusa mifupa ya Elisha, alifufuka na kusimama wima. Mfalme Hazaeli wa Aramu aliwanyanyasa sana watu wa Israeli wakati wote wa enzi ya Yehoahazi. Lakini Mwenyezi-Mungu aliwarehemu na kuwaonea huruma. Aliwaangalia kwa wema kwa sababu ya agano lake na Abrahamu, Isaka na Yakobo. Hakuwaangamiza wala hajawaacha kamwe mpaka leo. Hazaeli mfalme wa Aramu alipofariki, Ben-hadadi mwanawe alitawala mahali pake. Mfalme Yehoashi alimshinda Ben-hadadi mara tatu na kuikomboa miji yote iliyotekwa wakati wa utawala wa Yehoahazi, baba yake Yehoashi. Katika mwaka wa pili wa enzi ya Yehoashi mwana wa Yehoahazi huko Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alipoanza kutawala alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano, naye alitawala katika Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu. Alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwa kama babu yake Daudi. Bali alifanya mambo yote kama Yoashi baba yake; isipokuwa mahali pa ibada milimani hapakuharibiwa na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani mahali hapo. Mara tu Amazia alipojiimarisha mamlakani, aliwaua watumishi waliomuua mfalme, baba yake. Lakini hakuwaua watoto wa wauaji; kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria za Mose, Mwenyezi-Mungu anapotoa amri akisema, “Wazazi hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya wazazi wao; bali kila mtu atauawa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.” Amazia aliwaua Waedomu 10,000 katika Bonde la Chumvi; aliutwaa kwa nguvu mji wa Sela na kuuita Yoktheeli, na hivi ndivyo unavyoitwa mpaka sasa. Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu mfalme wa Israeli akisema, “Njoo tupambane.” Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli alimpelekea ujumbe Amazia mfalme wa Israeli, akisema, “Siku moja mbaruti wa Lebanoni uliuambia mwerezi, wa huko Lebanoni pia, ‘Mwoze binti yako kwa mwanangu.’ Lakini mnyama wa mwituni akapita hapo na kuukanyagakanyaga mbaruti huo. Sasa wewe Amazia umewashinda kabisa Waedomu, na moyo wako unakufanya ujivune. Ridhika na utukufu wako, ukakae nyumbani; ya nini kujitafutia taabu zitakazokuangamiza wewe mwenyewe pamoja na watu wako wa Yuda?” Lakini Amazia hakujali. Kwa hiyo Yehoashi mfalme wa Israeli alitoka akakabiliana uso kwa uso na Amazia huko vitani Beth-shemeshi, nchini Yuda. Watu wa Yuda walishindwa na watu wa Israeli na kila mmoja alirudi kwake. Yehoashi mfalme wa Israeli alimteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yehoashi, mwana wa Ahazia huko Beth-shemeshi; halafu akauendea Yerusalemu na kuubomoa ukuta wake kutoka Lango la Efraimu mpaka Lango la Pembeni, umbali wa karibu mita 200. Alichukua dhahabu yote na fedha, hata na vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu; pia alichukua mateka, kisha akarudi Samaria. Matendo mengine yote ya Yehoashi, ushujaa wake na vita alivyopigana na mfalme Amazia wa Yuda yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Yehoashi alifariki, akazikwa katika makaburi ya kifalme huko Samaria. Mwanae, Yeroboamu akatawala mahali pake. Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya mfalme Yehoashi wa Israeli kufariki. Matendo mengine yote ya Amazia yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Njama za kumwua Amazia zilifanywa Yerusalemu, kwa hiyo alikimbilia Lakishi, lakini maadui walituma watu wa kumwua huko. Maiti yake ililetwa juu ya farasi na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika Yerusalemu katika mji wa Daudi. Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria akiwa na umri wa miaka kumi na sita, wakamtawaza mahali pa Amazia baba yake. Azaria, baada ya kifo cha baba yake, aliujenga upya mji wa Elathi na kuurudisha kwa Yuda. Katika mwaka wa kumi na tano wa enzi ya Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala huko Samaria, akatawala kwa muda wa miaka arubaini na mmoja. Alimwasi Mwenyezi-Mungu akafuata mfano wa mtangulizi wake mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Aliikomboa nchi yote iliyokuwa mali ya Israeli, kutoka Pito la Hamathi mpaka Bahari ya Araba. Hivi ndivyo alivyoahidi Mwenyezi-Mungu kwa njia ya mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii, kutoka Gath-heferi. Maana Mwenyezi-Mungu aliona taabu kubwa kwa waliyopata Waisraeli kwani hapakuwa na mtu yeyote wa kuwasaidia. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwa amesema ya kwamba ataangamiza Israeli kabisa, hivyo aliwaokoa kwa njia ya mfalme Yeroboamu mwana wa Yehoashi. Matendo mengine yote ya Yeroboamu, vita alivyopigana kwa ushujaa, na jinsi alivyoikomboa Damasko na Hamathi na kuifanya mali ya Israeli, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Yeroboamu alifariki na kuzikwa katika makaburi ya kifalme na mwanawe Zekaria akatawala mahali pake. Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Azaria mwana wa Amazia mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Yekolia wa Yerusalemu. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu sawasawa na yote baba yake aliyotenda. Hata hivyo, mahali pa ibada milimani hapakuharibiwa, na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani hapo. Mwenyezi-Mungu akamwadhibu Azaria, akawa na ukoma mpaka alipokufa. Alikaa katika nyumba ya pekee na shughuli zake zote za utawala ziliendeshwa na mwanawe Yothamu. Matendo mengine yote ya Azaria yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Azaria alifariki na kuzikwa katika makaburi ya wafalme katika mji wa Daudi; na mwanawe Yothamu alitawala mahali pake. Katika mwaka wa thelathini na nane wa enzi ya Azaria mfalme wa Yuda, Zekaria mwana wa Yeroboamu alianza kutawala Israeli, akatawala kwa muda wa miezi sita. Naye, kama vile watangulizi wake, alimwasi Mwenyezi-Mungu. Alifuata mfano mbaya wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Shalumu mwana wa Yabeshi alikula njama dhidi ya mfalme Zekaria, akampiga mbele ya watu na kumwua, kisha akatawala mahali pake. Matendo mengine yote ya Zekaria yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Basi tukio hilo lilitokana na ahadi ya Mwenyezi-Mungu kwa mfalme Yehu, kusema, “Wazawa wako watatawala Israeli mpaka kizazi cha nne.” Katika mwaka wa thelathini na tisa wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Shalumu mwana wa Yabeshi alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa mwezi mmoja. Menahemu mwana wa Gadi aliondoka Tirza kwenda Samaria, na huko akamuua Shalumu mwana wa Yabeshi, kisha akatawala mahali pake. Matendo mengine yote ya Shalumu na njama zake zote alizofanya, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Menahemu alipokuwa njiani kutoka Tirza, aliuharibu kabisa mji wa Tapua na kuangamiza wakazi wake pamoja na nchi yote iliyozunguka kwa sababu hawakujisalimisha kwake. Isitoshe, aliwatumbua wanawake waja wazito wote. Katika mwaka wa thelathini na tisa wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa miaka kumi. Alimwasi Mwenyezi-Mungu siku zote za utawala wala hakuacha maovu ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Basi, Pulu mfalme wa Ashuru, aliivamia Israeli, naye Menahemu akampa kilo thelathini na nne za fedha ili amsaidie kuimarisha mamlaka yake juu ya nchi ya Israeli. Menahemu alipata fedha hiyo kwa kuwalazimisha matajiri wa Israeli kutoa mchango wa shekeli hamsini za fedha kila mmoja. Halafu Pulu hakukaa Israeli bali alirudi katika nchi yake. Matendo mengine yote ya Menahemu yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Menahemu alifariki, naye mwanawe Pekahia alitawala mahali pake. Katika mwaka wa hamsini wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa miaka miwili. Alimwasi Mwenyezi-Mungu na kufuata mfano mbaya wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Peka mwana wa Remalia, ambaye alikuwa ofisa wa jeshi la Pekahia, alishirikiana na watu wengine hamsini kutoka Gileadi, akamuua Pekahia katika ngome ya ndani ya nyumba ya mfalme huko Samaria, na kuwa mfalme mahali pake. Matendo mengine ya Pekahia na yote aliyofanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Katika mwaka wa hamsini na mbili wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Peka mwana wa Remalia alianza kutawala huko Samaria, akatawala kwa muda wa miaka ishirini. Alimwasi Mwenyezi-Mungu kwa kufuata mfano mbaya wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewafanya watu wa Israeli watende dhambi. Wakati wa enzi ya Peka mfalme wa Israeli, Tiglath-pileseri, mfalme wa Ashuru, aliteka miji ya Iyoni, Abel-beth-maaka, Yanoa, Kadeshi na Hazori, pamoja na nchi za Gileadi, Galilaya na Naftali na kuwachukua mateka wakazi wao. Katika mwaka wa ishirini wa utawala wa Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela alikula njama dhidi ya Peka, mwana wa Remalia, na akamuua, kisha akatawala mahali pake. Matendo mengine ya Peka na yote aliyoyafanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Katika mwaka wa pili wa enzi ya Peka mwana wa Remalia huko Israeli, Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda alianza kutawala Yuda. Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha, binti Sadoki. Kama vile Uzia baba yake, Yothamu alitenda mambo yaliyompendeza Mwenyezi-Mungu. Hata hivyo, mahali pa kuabudia miungu ya uongo hapakuharibiwa, na watu waliendelea kutoa sadaka na kufukiza ubani kwenye mahali pa juu. Yothamu alijenga lango la kaskazini la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Matendo mengine ya Yothamu na yote aliyofanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Wakati wa enzi ya Yothamu, Mwenyezi-Mungu alianza kutuma mfalme Resini wa Aramu na mfalme Peka wa Israeli ili kushambulia Yuda. Yothamu akafariki na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi. Mwanae Ahazi alitawala mahali pake. Katika mwaka wa kumi na saba wa enzi ya Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli, Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu. Hakufanya mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama Daudi babu yake alivyofanya, bali alifuata mienendo ya wafalme wa Israeli. Isitoshe, hata alimpitisha mwanawe motoni kuwa tambiko, akifuata desturi mbaya za mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini. Ahazi alitoa sadaka na kufukiza ubani mahali pa juu, vilimani na chini ya kila mti mbichi. Kisha Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walitokea ili kupigana vita dhidi ya Yerusalemu, nao walimzingira Ahazi, lakini hawakuweza kumshinda. (Wakati huo, mfalme wa Edomu aliuteka akawarudishia Waedomu mji wa Elathi na kuwafukuza watu wa Yuda waliokaa humo. Nao Waedomu wakaingia Elathi na kufanya makao yao huko mpaka sasa.) Basi Ahazi akatuma watu kwa mfalme Tiglath-pileseri wa Ashuru wakiwa na ujumbe huu: “Mimi ni mtumishi wako mwaminifu. Njoo uniokoe kutoka kwa wafalme wa Aramu na Israeli ambao wananishambulia.” Ahazi akachukua fedha na dhahabu iliyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na hazina iliyokuwa katika nyumba ya mfalme na kumpelekea kama zawadi mfalme wa Ashuru. Tiglath-pileseri, akiitikia ombi la Ahazi, aliushambulia mji wa Damasko na kuuteka. Akamuua mfalme Resini na kuwapeleka mateka Kiri. Mfalme Ahazi alipokwenda Damasko kukutana na mfalme Tiglath-pileseri, aliona madhabahu huko. Basi, akamtumia kuhani Uria mfano kamili na mchoro wa madhabahu hiyo. Uria akajenga madhabahu hiyo kulingana na mfano huo na kuimaliza kabla ya Ahazi kurejea nyumbani. Ahazi aliporejea kutoka Damasko, aliiona hiyo madhabahu; basi akaikaribia madhabahu na kutoa sadaka juu yake. Alitoa sadaka yake ya kuteketezwa, ya nafaka, na ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka ya amani. Madhabahu ya shaba ambayo iliwekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, aliiondoa mbele ya nyumba kutoka nafasi yake katikati ya madhabahu yake na nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaiweka kwenye nafasi iliyokuwa upande wa kaskazini wa madhabahu yake. Kisha alimwamuru Uria, “Tumia hii madhabahu yangu kubwa kwa kuteketeza sadaka za asubuhi na sadaka za nafaka za jioni, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka za mfalme na za watu wote na pia sadaka za divai za watu. Irashie damu ya wanyama wote wa kuteketezwa ambao wametolewa sadaka. Lakini ile madhabahu ya shaba nitaitumia mimi kwa kuuliza kauli ya Mungu.” Naye Uria akafuata maagizo ya mfalme. Mfalme Ahazi aliziondoa papi zilizokuwa zimesimamishwa huko, akaondoa birika lililoitwa bahari ambalo lilikuwa juu ya wale fahali kumi na wawili wa shaba na kuliweka juu ya msingi wa mawe. Nalo jukwaa lililotumika siku ya Sabato lililokuwa limejengwa ndani ya nyumba pamoja na kivutio cha nje, mfalme alivihamisha kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya mfalme wa Ashuru. Matendo mengine yote ya mfalme Ahazi yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Ahazi akafa na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi, naye Hezekia mwanawe akatawala mahali pake. Katika mwaka wa kumi na mbili wa enzi ya mfalme Ahazi wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka tisa. Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu ingawa siyo kama wafalme wa Israeli waliomtangulia. Mfalme Shalmanesa wa Ashuru alimshambulia; naye Hoshea akawa mtumishi wake na kumlipa ushuru. Lakini wakati mmoja Hoshea alituma wajumbe kwa mfalme wa Misri akiomba msaada; ndipo akaacha kulipa ushuru kwa mfalme Shalmanesa wa Ashuru kama alivyozoea kufanya kila mwaka. Shalmanesa alipoona hivi alimfunga Hoshea kwa minyororo na kumweka gerezani. Kisha mfalme wa Ashuru akaivamia nchi nzima na kuufikia mji wa Samaria na kuuzingira kwa muda wa miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Hoshea, mfalme wa Ashuru aliuteka Samaria, na kuwachukua watu wa Israeli mateka mpaka Ashuru, baadhi yao akawaweka katika mji wa Hala, wengine karibu na mto Habori, mto Gozani na wengine katika miji ya Media. Haya yote yalitendeka kwa sababu watu wa Israeli walimwasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, ambaye aliwatoa kutoka mikononi mwa mfalme wa Misri, pia waliabudu miungu mingine, na kufuata njia za mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli, na kufanya matendo ya wafalme wa Israeli waliyoyaingiza nchini. Watu wa Israeli walitenda kwa siri mambo yasiyokuwa mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walijenga mahali pa juu pa kuabudia miungu ya uongo katika kila mji, kuanzia mnara wa walinzi mashambani hadi katika mji wenye ngome. Juu ya kila kilima na chini ya kila mti wenye majani mabichi, walijenga nguzo za mawe na sanamu za mungu wa kike Ashera, na wakafukiza ubani kwenye madhabahu zote za miungu ya uongo kufuatia desturi za mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa matendo yao maovu, na walitumikia sanamu ambazo Mwenyezi-Mungu alikuwa amewakataza, akisema, “Msifanye hivyo.” Mwenyezi-Mungu alituma manabii na waonaji kuionya Israeli na Yuda akisema, “Acheni njia zenu mbaya mkatii amri zangu na maagizo yangu kufuatana na sheria nilizowapa babu zenu, na ambazo niliwapeni kupitia kwa watumishi wangu manabii.” Lakini wao hawakutii; walikuwa wagumu kama babu zao ambao hawakumwamini Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walikataa kutii maagizo yake; hawakushika agano alilofanya na babu zao; licha ya kupuuza maonyo yake, waliabudu sanamu zisizokuwa na maana mpaka hata wao wenyewe hawakuwa na maana tena; walifuata desturi za mataifa yaliyowazunguka: Walipuuza amri za Mwenyezi-Mungu; wala hawakuzizingatia. Walivunja amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakatengeneza sanamu za miungu ya ndama wawili wa kusubu; vilevile wakatengeneza sanamu za mungu wa kike Ashera wakaabudu na vitu vyote vya angani na wakamtumikia Baali. Waliwatambika watoto wao wa kiume na wa kike kwa miungu ya uongo; wakataka shauri kwa watabiri na wachawi. Walinuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakamkasirisha sana. Basi, Mwenyezi-Mungu akawakasirikia sana watu wa Israeli na kuwafukuza kabisa mbele yake; hakuacha mtu isipokuwa kabila la Yuda peke yake. Lakini hata watu wa Yuda hawakutii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao; bali walifuata desturi zilizoletwa na watu wa Israeli. Mwenyezi-Mungu aliwakataa Waisraeli wote; akawaadhibu na kuwaacha mikononi mwa adui wakali, na kisha akawafukuza mbele yake. Baada ya Mwenyezi-Mungu kutenga watu wa Israeli kutoka ukoo wa Daudi, walimtawaza Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme. Naye Yeroboamu aliwafanya watu wa Israeli kumwacha Mwenyezi-Mungu na kutenda dhambi kubwa sana. Waisraeli walitenda dhambi alizotenda Yeroboamu; hawakuweza kuziacha, hadi hatimaye Mwenyezi-Mungu akawafukuza kutoka mbele yake, kama vile alivyokuwa amesema kupitia kwa watumishi wake wote manabii. Kwa hiyo watu wa Israeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe mpaka Ashuru ambako wanakaa hata sasa. Kisha mfalme wa Ashuru akachukua watu kutoka Babuloni, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria mahali pa watu wa Israeli waliopelekwa uhamishoni. Wakaitwaa miji hiyo na kukaa humo. Basi ilitokea kwamba walipoanza kukaa humo, hawakumwabudu Mwenyezi-Mungu, kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akatuma simba miongoni mwao, nao wakawaua baadhi yao. Halafu watu walimwambia mfalme wa Ashuru, “Mataifa uliyochukua na kuyaweka katika miji ya Samaria hayakujua hukumu za Mungu wa nchi hiyo, kwa hiyo Mungu huyo alituma simba ambao wanawaua.” Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru, “Mrudishe kuhani mmoja kati ya wale tuliowaleta mateka; mrudishe aende na kukaa huko, ili awafundishe watu sheria ya Mungu wa nchi hiyo.” Kwa hiyo mmoja wa makuhani waliotekwa nyara toka Samaria alikwenda na kukaa Betheli, na huko aliwafundisha watu jinsi ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Lakini mataifa yote katika miji yalimoishi yalijitengenezea miungu yao na kuiweka mahali pa juu ambako watu wa Samaria walikuwa wametengeneza. Watu wa Babuloni walitengeneza vinyago vya Sukoth-benothi; Wakuthi vinyago vya Nergali; Wahamathi vinyago vya Ashima; Waiva vinyago vya Nibhazi na Tartaki; na Wasefarvaimu walitoa watoto wao kuwa sadaka za kuteketezwa kwa miungu yao Adrameleki na Anameleki. Watu hawa vilevile walimwabudu Mwenyezi-Mungu. Waliteua kutoka kati yao watu wa kila aina na kuwafanya makuhani kutumika katika mahali pa juu na kutoa sadaka huko kwa niaba yao. Hivi walimwabudu Mwenyezi-Mungu, lakini wakati huohuo waliwaabudu pia miungu yao waliyoichukua kutoka nchi zao. Hata sasa wanatenda kama walivyofanya hapo awali. Hawamwabudu Mwenyezi-Mungu, na wala hawafuati masharti, maagizo, sheria au amri ambazo yeye Mwenyezi-Mungu aliwaamuru wana wa Yakobo; ambaye alimpa jina Israeli. Mwenyezi-Mungu alikuwa amefanya agano nao na kuwaamuru, “Msiabudu miungu mingine; msiisujudie, msiitumikie wala msiitambikie. Mtaniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, ambaye niliwatoa huko Misri kwa uwezo na nguvu nyingi. Mtanisujudia mimi na kunitolea sadaka. Wakati wote mtatii masharti, maongozi, sheria na amri ambazo niliandika kwa ajili yenu, siku zote mtakuwa waangalifu kuzitenda. Msiiabudu miungu mingine, wala msisahau agano nililofanya nanyi; msiiabudu miungu mingine, bali mtaniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nami nitawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu.” Lakini watu hao hawakusikiliza, bali waliendelea kutenda kama walivyofanya hapo awali. Basi mataifa haya yalimwabudu Mwenyezi-Mungu, lakini pia yalitumikia sanamu zao za kusubu; na mpaka sasa hivi, wazawa wao wanaendelea kutenda hivyo kama walivyotenda babu zao. Katika mwaka wa tatu wa enzi ya Hoshea mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Hezekia mwana wa Ahazi, mfalme wa Yuda, alianza kutawala; alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala. Alitawala miaka ishirini na tisa huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Abi, binti wa Zekaria. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama alivyofanya Daudi babu yake. Aliharibu mahali pote pa juu pa kuabudia miungu ya uongo na kuvunja nguzo za kutambikia na za mungu Ashera. Kadhalika, alivunja nyoka wa shaba ambaye Mose alimtengeneza, aliyeitwa Nehushtani. Mpaka wakati huo, watu wa Israeli walikuwa wakiitambikia. Hezekia alimtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli; hakuna aliyekuwa kama yeye kati ya wafalme wa Yuda waliomfuata au waliomtangulia. Yeye hakumwasi Mwenyezi-Mungu wala hakuacha kumfuata, bali alishika amri za Mwenyezi-Mungu alizomwamuru Mose. Basi, Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye, na alimfanya kufaulu kwa kila alilotenda. Alimwasi mfalme wa Ashuru na kukataa kumtumikia. Aliwapiga Wafilisti mpaka mji wa Gaza na nchi iliyouzunguka, kuanzia mnara wa walinzi mpaka mji wenye ngome. Katika mwaka wa nne wa enzi ya Hezekia, ambao pia ulikuwa mwaka wa saba wa enzi ya Hoshea mwana wa Ela mfalme wa Israeli, Shalmanesa mfalme wa Ashuru alishambulia mji wa Samaria na kuuzingira. Mwishoni mwa mwaka wa tatu Waashuru waliuteka Samaria. Ilikuwa katika mwaka wa sita wa enzi ya Hezekia na pia mwaka wa tisa wa enzi ya Hoshea mfalme wa Israeli, Samaria ulipotekwa. Mfalme wa Ashuru aliwachukua watu wa Israeli mateka mpaka Ashuru na kuwaweka wengine wao katika mji wa Hala, na karibu ya Habori, mji wa Gozani, pia na wengine katika miji ya Media, kwa sababu Waisraeli hawakutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, bali walivunja agano lake, hata hawakusikia wala kutii yote Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliyowaamuru. Mnamo mwaka wa kumi na nne wa utawala wa mfalme Hezekia, mfalme Senakeribu wa Ashuru aliishambulia miji yote yenye ngome ya Yuda na kuiteka. Hezekia akatuma ujumbe kwa Senakeribu huko Lakishi na kumwambia, “Nimefanya makosa. Tafadhali, komesha mashambulio yako kwangu; nami nitalipa chochote utakacho.” Mfalme wa Ashuru akaagiza Hezekia amletee tani kumi za fedha na tani moja ya dhahabu. Hezekia akampelekea fedha yote iliyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina za nyumba ya mfalme; kadhalika, alingoa dhahabu kutoka katika milango ya hekalu la Mwenyezi-Mungu na ile dhahabu ambayo yeye mwenyewe aliiweka kwenye mihimili ya mlango; yote akampelekea Senakeribu. Kisha mfalme wa Ashuru alimtuma jemadari mkuu, amiri mkuu, mkuu wa matowashi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi kwenda kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Walisafiri na kufika Yerusalemu. Nao walipowasili waliingia na kusimama karibu na mfereji wa bwawa lililoko upande wa juu katika barabara kuu inayoelekea Uwanda wa Dobi. Walipomwita mfalme Hezekia walilakiwa na Eliakimu mwana wa Hilkia, ambaye alikuwa msimamizi wa ikulu; Shebna, aliyekuwa katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wa kumbukumbu za mfalme. Ndipo jemadari mkuu alipowaambia, “Mwambieni Hezekia, hivi ndivyo anavyosema mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni ujasiri wa namna gani huu unaouwekea matumaini? Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi? Angalia, sasa, unategemea Misri, utete uliovunjika ambao utamchoma mkono yeyote atakayeutegemea. Hivyo ndivyo Farao mfalme wa Misri alivyo kwa wote wale wanaomtegemea.” “Lakini hata kama mkiniambia: ‘Tunamtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu’, Jueni kwamba ni Mungu huyohuyo ambaye Hezekia alipaharibu mahali pake pa juu na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu waabudu tu mbele ya madhabahu iliyoko Yerusalemu. Basi, fanyeni mkataba na bwana wangu mfalme wa Ashuru, nami nitawapa farasi 2,000 kama mtaweza kupata wapandafarasi. Mwawezaje kumrudisha nyuma ofisa mmoja kati ya watumishi wa bwana wangu walio na cheo cha chini kabisa, wakati mnategemea Misri iwaletee magari na wapandafarasi?” Zaidi ya hayo, je, mnafikiri nimekuja bila amri ya Mwenyezi-Mungu ili kuishambulia na kuiangamiza nchi hii? Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeniambia, “Ishambulie nchi hii na kuiangamiza!” Basi, Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia huyo jemadari mkuu, “Tafadhali, sema nasi kwa lugha ya Kiaramu, maana tunaielewa; usiseme nasi kwa lugha ya Kiebrania; kwa kuwa watu walioko ukutani wanasikiliza.” Yule jemadari mkuu akawaambia, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu wanaokaa ukutani ambao wamehukumiwa pamoja nanyi kula mavi yao wenyewe na kunywa mikojo yao wenyewe?” Kisha huyo mkuu wa matowashi akasimama, akapaza sauti na kusema kwa lugha ya Kiebrania, “Sikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! Hivi ndivyo anavyosema mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye, kwa sababu hataweza kuwaokoa mikononi mwa mfalme. Msikubali awashawishi ili mumtegemee Mwenyezi-Mungu akisema, ‘Mwenyezi-Mungu atatuokoa na mji huu hautatiwa mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’ Msimsikilize Hezekia, maana mfalme wa Ashuru anasema, ‘Muwe na amani nami, na jisalimisheni kwangu. Hapo kila mmoja wenu ataweza kula matunda ya mzabibu wake mwenyewe, matunda ya mtini wake mwenyewe, na kunywa maji ya kisima chake mwenyewe, mpaka baadaye nitakapokuja na kuwapeleka mbali katika nchi kama hii yenu, nchi yenye nafaka na divai, nchi yenye mikate na mashamba ya mizabibu; nchi yenye mizeituni na asali, ili mpate kuishi, msije mkafa.’ Msimsikilize Hezekia anapowahadaa akisema, ‘Mwenyezi-Mungu atatuokoa.’ Je, kuna yeyote kati ya miungu ya mataifa aliyeokoa nchi yake kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru? Je, iko wapi miungu ya Hamathi na Arpadi. Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena na Iva? Je, imeokoa Samaria mikononi mwangu? Ni nani miongoni mwa miungu ya nchi hizi aliyeokoa nchi zao mikononi mwangu hata Mwenyezi-Mungu aweze kuukoa mji wa Yerusalemu?” Lakini watu wote walinyamaza kimya, wala hawakumjibu neno, kama walivyoamriwa na mfalme Hezekia, akisema, “Msimjibu.” Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi, wakamwendea Hezekia huku mavazi yao yakiwa yameraruka, wakamweleza maneno ya jemadari mkuu. Mfalme Hezekia alipopata habari hizo, alirarua mavazi yake, akavaa gunia akaingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia. Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama ambaye anataka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa. Inawezekana Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya jemadari mkuu, ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai; naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atakaripia maneno aliyosikia. Kwa hiyo waombee watu waliobaki.’” Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya, aliwaambia “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Usiogope kwa sababu ya maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wameyasema kunikebehi. Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi, halafu atarudi katika nchi yake na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’” Kisha yule jemadari mkuu aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akiushambulia mji wa Libna. Halafu mfalme alipopata habari kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi anakuja kupigana naye, alituma wajumbe kwa Hezekia, akisema, “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda, ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba mji wa Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru. Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, wadhani wewe utaokoka? Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, na Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo babu zangu waliyaangamiza? Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na wa Iva?’” Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akaiweka mbele yake Mwenyezi-Mungu. Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, unayekaa katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa, ni wewe tu uliye Mungu, unayetawala falme zote za ulimwengu. Wewe uliumba nchi na mbingu. Ee Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka kukutukana wewe Mungu uliye hai. Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa na nchi zao. Walitupa miungu yao motoni kwa sababu haikuwa miungu ya kweli, bali sanamu za miti na mawe zilizochongwa na mikono ya watu. Sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, nakusihi utuokoe makuchani mwa Senakeribu, falme zote za dunia zijue kwamba ni wewe peke yako, ee Mwenyezi-Mungu, uliye Mungu.” Kisha Isaya, mwana wa Amozi akatuma ujumbe kwa Hezekia, akisema, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ‘Nimesikia ombi lako kwangu kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru:’ Hili ndilo neno la Mwenyezi-Mungu alilosema kumhusu Senakeribu: Anakudharau, anakubeza binti Siyoni, anatikisa kichwa chake nyuma yako binti Yerusalemu. Je, uliyekuwa unamkashifu na kumdhihaki ni nani? Nani umemwinulia sauti na kumkodolea macho kwa kiburi? Juu ya Mtakatifu wa Israeli!” Kwa kuwatuma wajumbe wako umemkashifu Bwana, wewe umesema, “Kwa magari yangu mengi ya vita, nimekwea vilele vya milima mpaka kilele cha Lebanoni. Nimekata mierezi yake mirefu, na misonobari mizurimizuri; nimeingia mpaka ndani yake na ndani ya misitu yake mikubwa. Nimechimba visima na kunywa maji mageni nilikausha mito yote ya Misri kwa nyayo za miguu yangu. ‘Je, hujasikia, kwamba nilipanga jambo hili tangu awali? Ninachotekeleza sasa nilikipanga zamani.’ Nilikuweka uijenge miji yenye ngome kwa rundo la magofu. Wakazi wake wakiwa wameishiwa nguvu, wametishika na kufadhaika, wamekuwa kama mimea ya shambani, kama majani yasiyo na nguvu. Kama majani yaotayo juu ya paa; yakaukavyo kabla ya kukua. Najua kuketi kwako, na kuamka kwako nako kuingia kwako; nayo mipango yako dhidi yangu. Kwa vile umefanya mipango dhidi yangu na nimeusikia ufidhuli wako, nitatia ndoana yangu puani mwako, na lijamu yangu kinywani mwako. Nitakurudisha njia ileile uliyojia.” Kisha Isaya akamwambia mfalme Hezekia, “Na hii ndio itakuwa ishara kwako Hezekia: Mwaka huu na mwaka ujao mtakula kinachomea chenyewe bila kupandwa. Lakini katika mwaka wa tatu mtapanda na kuvuna mavuno; mtapanda mizabibu na kula matunda yake. Wale watakaobaki katika ukoo wa Yuda wataongezeka na kuwa wengi kama vile mti unavyotoa mizizi yake udongoni na kuzaa matunda juu. Maana kutakuwako watu watakaosalia huko Yerusalemu; naam, huko mlimani Siyoni kutakuwako watu wachache watakaosalimika; maana Mwenyezi-Mungu amedhamiria kukamilisha hayo. “Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya mfalme wa Waashuru: ‘Hataingia katika mji huu wala kuupiga mshale wala kuujia kwa ngao wala kuuzingira. Atarudi kwa njia ileile aliyoijia na wala hataingia katika mji huu,’ ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu. ‘Naam, kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi nitaulinda na kuokoa mji huu.’” Basi, usiku huo malaika wa Mwenyezi-Mungu aliingia kambini mwa Waashuru na kuwaua watu laki moja. Kulipopambazuka watu wakaamka, hao wote walionekana wakiwa maiti. Kisha Senakeribu mfalme wa Ashuru aliondoka akaenda zake na kukaa Ninewi. Siku moja wakati Senakeribu alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki mungu wake, wanawe wawili, Adrameleki na Sharezeri walimuua kwa upanga, halafu wakakimbilia nchini Ararati. Naye Esar-hadoni, mwanawe akatawala badala yake. Wakati huo Hezekia aliugua sana karibu na kufa. Ndipo nabii Isaya, mwana wa Amozi alipomwendea na kumwambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu; ‘Panga mambo yako sawasawa katika nyumba yako kwa kuwa utakufa, hutapona.’” Hezekia akageukia upande wa ukuta na kumwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi ukumbuke jinsi nilivyokutumikia kwa uaminifu na kwa moyo wangu wote na kutenda yaliyo sawa mbele yako.” Hezekia akalia kwa uchungu sana. Lakini kabla Isaya hajapita ua wa katikati, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia, kusema, “Rudi ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wa Mwenyezi-Mungu: Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu yako Daudi, nimesikia ombi lako na nimeona machozi yako. Nitakuponya na baada ya siku tatu utakwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nitakuongezea miaka kumi na mitano ya kuishi. Nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mikononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi.” Basi Isaya akasema, “Leteni andazi la tini mliweke kwenye jipu lake, ili apate kupona.” Hezekia akamwuliza Isaya, “Ni ishara gani ambayo itanionesha kwamba kweli Mwenyezi-Mungu ataniponya na katika siku ya tatu nitaweza kwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu?” Isaya akamjibu, “Hii itakuwa ishara kwako kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, kwamba Mwenyezi-Mungu atafanya kama alivyoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele au nyuma?” Hezekia akamjibu, “Ni rahisi zaidi kivuli kwenda mbele hatua kumi! Hebu kirudi nyuma hatua kumi.” Isaya akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akafanya kivuli kirudi hatua kumi kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi. Wakati huo, mfalme Merodak-baladani mwana wa Baladani mfalme wa Babuloni alisikia kuwa Hezekia alikuwa ameugua na sasa amepona, akamtumia ujumbe pamoja na zawadi. Basi, Hezekia akawakaribisha na kuwaonesha mali yake: Nyumba yake ya hazina, fedha, dhahabu, viungo vya kukolezea chakula, mafuta ya thamani na nyumba ya vifaa vyake vyote vya kijeshi na vitu vyote vilivyokuwamo katika bohari zake. Hakukuwa chochote katika ikulu yake, au nchi yake ambacho hakuwaonesha. Ndipo nabii Isaya alipomwendea mfalme Hezekia na kumwuliza, “Watu hawa wamesema nini? Na, wamekujia kutoka wapi?” Naye Hezekia akamjibu, “Wamenijia kutoka nchi ya mbali.” Halafu akamwuliza, “Wameona nini katika ikulu yako?” Hezekia akamjibu, “Wameona yote yaliyomo katika ikulu yangu. Hakuna chochote katika bohari zangu ambacho sikuwaonesha.” Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi-Mungu: Tazama, siku zinakuja ambapo vyote vilivyomo nyumbani mwako na vitu vyote walivyokusanya baba zako mpaka wakati huu vitapelekwa mpaka Babuloni. Hakuna kitu chochote kitakachobaki; ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu. Tena baadhi ya watoto wako wa kiume watapelekwa mateka, nao watakuwa matowashi katika ikulu ya mfalme wa Babuloni.” Naye Hezekia akamwambia Isaya, “Neno la Mwenyezi-Mungu kama ulivyolisema ni sawa.” Alisema hivyo kwani alifikiri, “Kwa nini isiwe hivyo, ikiwa kutakuwapo amani na ulinzi katika siku za utawala wangu.” Matendo mengine ya Hezekia, ushujaa wake na maelezo juu ya jinsi alivyojenga bwawa na kuchimba mfereji wa kuleta maji mjini, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Hezekia alifariki, naye Manase mwanawe akatawala mahali pake. Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala Yuda, akatawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa miaka hamsini na mitano. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kuiga mienendo miovu ya mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu wakati watu wake, Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini. Kwa maana alirekebisha mahali pa kuabudia miungu mingine palipoharibiwa na Hezekia baba yake; akajenga madhabahu za kuabudia Baali na kutengeneza sanamu ya Ashera, kama vile alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Isitoshe, Manase aliabudu na kutumikia vitu vyote vya mbinguni. Alijenga madhabahu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema, “Jina langu litaabudiwa katika Yerusalemu.” Katika nyua mbili za nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alijenga madhabahu ya kuabudia sayari. Pia alimtoa mwanawe kuwa sadaka ya kuteketezwa. Alipiga ramli; alibashiri akishirikiana na waaguzi wa mizimu na wachawi. Alitenda maovu mengi mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamkasirisha. Nayo sanamu ya Ashera aliyotengeneza akaiweka katika nyumba ambayo Mwenyezi-Mungu aliizungumzia mbele ya Daudi na mwanawe Solomoni: “Katika nyumba hii na mjini Yerusalemu niliouchagua ndiko mahali nitakapoabudiwa milele. Na iwapo Waisraeli watajali kutenda yote niliyowaamuru na kufuata Sheria zote mtumishi wangu Mose alizowapa, basi sitawaacha wafukuzwe kutoka katika nchi hii ambayo niliwapa babu zao.” Lakini hawakusikia, naye Manase aliwafanya watende dhambi zaidi kuliko zile zilizofanywa na mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyaharibu mbele ya Waisraeli. Ndipo Mwenyezi-Mungu alisema kupitia kwa watumishi wake manabii, “Kwa sababu mfalme amefanya mambo ya kuchukiza, mambo mabaya zaidi ya yale yaliyotendwa na Waamori waliomtangulia, amewafanya watu wa Yuda pia watende dhambi kwa kutumia sanamu zake; basi, sasa, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tazama nitaleta juu ya Yerusalemu na Yuda, msiba ambao hata yeyote atakayesikia atashtuka. Nitauadhibu Yerusalemu kama vile nilivyofanya Samaria, na mfalme Ahabu na wazawa wake. Nitafuta Yerusalemu kama mtu afutavyo sahani iliyosafishwa na kuiinamisha. Nitawaacha hao watu wa urithi wangu watakaosalia na kuwakabidhi kwa adui zao; watakuwa mawindo na mateka kwa adui zao wote. Nitawatendea hayo yote kwa sababu wameniasi na kunikasirisha tangu wazee wao walipotoka Misri mpaka leo.” Zaidi ya hayo, licha ya dhambi yake alipowakosesha watu wa Yuda wakafanya dhambi kwa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Manase aliwaua watu wengi wasiokuwa na hatia, damu ilijaa toka upande mmoja mpaka upande mwingine wa Yerusalemu. Matendo mengine ya Manase na yote aliyotenda, pamoja na dhambi zake zote, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Manase alifariki na kuzikwa katika bustani ya nyumba yake mwenyewe, katika Bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akatawala mahali pake. Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; alitawala miaka miwili huko Yerusalemu. Jina la mama yake ni Meshulemethi, binti Haruzi wa Yothba. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama vile Manase baba yake alivyofanya. Alifuata njia yote aliyoiendea baba yake na kutumikia sanamu ambazo baba yake alizitumikia na kuziabudu. Alimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake, hakushika njia ya Mwenyezi-Mungu. Baadaye watumishi wa Amoni walikula njama na kumwua katika ikulu yake. Lakini watu wa Yuda wakawaua wote waliomuua Amoni. Kisha watu hao wa Yuda wakamtawaza Yosia mwanawe mahali pake. Matendo mengine yote ya Amoni yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Yuda. Amoni alizikwa kaburini katika bustani ya Uza; na Yosia mwanawe akatawala mahali pake. Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala huko Yerusalemu, akatawala kwa miaka thelathini na mmoja. Mama yake alikuwa Yedida, binti Adaya, mkazi wa mji wa Boskathi. Yosia alitenda mema na alimpendeza Mwenyezi-Mungu. Alifuata mfano wa mfalme Daudi aliyemtangulia, na kushika amri za Mwenyezi-Mungu kwa makini. Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, mfalme alimtuma katibu Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu akisema, “Nenda kwa kuhani mkuu Hilkia umwambie ahesabu zile fedha zilizoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambazo mabawabu walizikusanya kutoka kwa watu. Kiasi cha fedha hizo zipewe wasimamizi wa marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kulipa mishahara ya mafundi wanaofanya marekebisho, yaani maseremala, wajenzi na waashi. Kiasi kingine kitumike kununua mbao na mawe yaliyochongwa kwa ajili ya kurekebisha nyumba. Watu wanaosimamia ujenzi wasidaiwe kutoa hesabu ya matumizi ya fedha watakazokabidhiwa, kwa sababu wanazitumia kwa uaminifu.” Kisha kuhani mkuu Hilkia alimwambia katibu Shafani, “Nimekipata Kitabu cha Sheria katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Halafu Hilkia akampatia Shafani kitabu, naye akakisoma. Katibu Shafani, alimwendea mfalme na kutoa habari, akisema, “Watumishi wako wametoa fedha zilizopatikana katika nyumba halafu wamezikabidhi kwa mafundi wanaosimamia marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Kisha katibu Shafani, akamwambia mfalme, “Kuhani Hilkia amenipa kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme. Mfalme aliposikia maneno ya Kitabu cha Sheria, alirarua mavazi yake. Mara aliamuru kuhani Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani na Akbori mwana wa Mikaya pamoja na katibu Shafani na Asaya mtumishi wa mfalme, akisema, “Nendeni mkatafute shauri kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwa niaba yangu na watu wa Yuda wote kuhusu maneno ya kitabu hiki kilichopatikana kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imewaka juu yetu, maana babu zetu hawakutii maneno ya kitabu hiki, na kutimiza yote yaliyoandikwa kutuhusu.” Kwa hiyo kuhani Hilkia, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya, wote walikwenda kwa mama mmoja nabii jina lake Hulda aliyekuwa mke wa Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya hekalu. Wakati huo Hulda alikuwa anaishi katika mtaa wa pili wa Yerusalemu, nao wakazungumza naye. Basi akawaambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Mwambie huyo aliyewatuma kwangu, Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Nitaleta uovu juu ya mahali hapa na juu ya wakazi wake kama ilivyo katika kitabu kilichosomwa na mfalme wa Yuda. Kwa sababu wameniacha na kufukizia ubani miungu mingine na hivyo kunikasirisha kwa kazi zote za mikono yao, ghadhabu yangu dhidi ya Yerusalemu itawaka na haitaweza kutulizwa. Lakini kuhusu mfalme wa Yuda aliyewatuma kutafuta shauri la Mwenyezi-Mungu, mwambie kwamba, hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, juu ya maneno uliyoyasikia, Kwa kuwa umetubu na kunyenyekea mbele yangu, hata umerarua mavazi yako na kulia mbele yangu, hapo uliposikia niliyosema dhidi ya mahali hapa na dhidi ya wakazi wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nami pia nimekusikia. Kwa hiyo tazama, nitakukusanya pamoja na babu zako nawe utawekwa kaburini kwa amani, macho yako hayataona uovu nitakaouleta juu ya mahali hapa.’” Basi wajumbe wakamletea mfalme Yosia habari hizi. Kisha mfalme alituma wajumbe, nao wakamkusanyia viongozi wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Naye mfalme akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu akifuatana na watu wote wa Yuda na wakazi wote wa Yerusalemu, na makuhani pamoja na manabii, watu wote wadogo kwa wakubwa. Basi, akawasomea maneno ya kitabu cha agano kilichopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu mfalme akasimama karibu na nguzo na kufanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu, kumfuata Mwenyezi-Mungu, kushika amri zake, maamuzi na masharti yake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, kutenda maneno yote ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hicho cha agano. Watu wote wakaungana katika kufanya agano. Kisha Yosia akaamuru kuhani mkuu Hilkia na makuhani wasaidizi wake na mabawabu watoe katika hekalu la Mwenyezi-Mungu vitu vilivyotengenezwa kwa ajili ya Baali, Ashera na kwa ajili ya sayari; aliviteketeza nje ya Yerusalemu katika bonde la Kidroni na kupeleka majivu yake huko Betheli. Kisha akawaondoa makuhani wote waliobarikiwa na wafalme wa Yuda ili kufukiza ubani katika mahali pa kuabudia katika miji ya Yuda na kuzunguka Yerusalemu; pia na wale waliofukiza ubani kwa Baali, jua, mwezi, nyota na sayari katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Aliondoa Ashera kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nje ya Yerusalemu, akaipeleka mpaka kijito cha Kidroni. Huko akaiteketeza na kuisaga mpaka ikawa mavumbi, nayo mavumbi yake akayatawanya juu ya makaburi ya watu. Alibomoa nyumba za mahanithi zilizokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, mahali ambamo wanawake walifuma mapazia ya Ashera. Akakusanya makuhani wote kutoka miji ya Yuda na akapatia najisi mahali pa juu makuhani walikofukiza ubani, kutoka Geba mpaka Beer-sheba; naye akabomoa mahali pa juu palipokuwa upande wa kushoto wa lango la mji penye malango yaliyokuwa kwenye njia ya kuingilia lango la Yoshua mtawala wa mji. Makuhani hao hawakufikia madhabahu ya Mwenyezi-Mungu katika Yerusalemu, lakini walikula mikate isiyotiwa chachu waliyopewa na jamaa zao. Mfalme Yosia pia alipatia najisi mahali pa kuabudia miungu ya uongo palipoitwa Tofethi katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu yeyote asimchome mwanawe au bintiye kuwa tambiko kwa Moleki. Kadhalika aliondoa farasi waliotengwa na wafalme wa Yuda kwa ajili ya jua, kwenye njia ya kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, karibu na chumba cha Nathan-meleki, kilichokuwa kiungani; naye alichoma kwa moto magari ya jua. Madhabahu ambayo wafalme wa Yuda walijenga paani kwenye chumba cha juu cha Ahazi, pamoja na madhabahu ambayo Manase alijenga katika nyua mbili za nyumba ya Mwenyezi-Mungu aliyabomoa na kuyapondaponda, kisha alitupa mavumbi yake katika kijito cha Kidroni. Mfalme pia alipatia unajisi mahali pa kuabudia palipokuwa upande wa mashariki ya Yerusalemu na kuelekea upande wa mlima wa Ufisadi, mahali mfalme wa Israeli alipopajenga kwa ajili ya Ashtarothi chukizo la Wasidoni, Kemoshi chukizo la Moabu na pia kwa ajili ya Milkomu chukizo la Waamoni. Alivunja nguzo katika vipandevipande; pia alikatakata sanamu za Ashera, na mahali zilipokuwa zinasimama alipajaza mifupa ya watu. Zaidi ya hayo aliharibu huko Betheli mahali pa kuabudia palipojengwa na mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewafanya watu wa Israeli watende dhambi; aliharibu madhabahu hayo na kuvunja mawe yake katika vipandevipande, na kisha akaviponda mpaka vikawa vumbi; pia akachoma sanamu ya Ashera. Kisha Yosia alipogeuka aliona makaburi juu ya kilima; aliagiza mifupa ifukuliwe kutoka makaburini na kuichoma juu ya madhabahu; basi akayatia unajisi madhabahu sawasawa na neno la Mwenyezi-Mungu ambalo mtu wa Mungu alilitangaza, nabii ambaye alitabiri matukio haya. Halafu mfalme aliuliza, “Mnara ninaouona kule ni wa nini?” Nao watu wa mji wakamjibu, “Ni kaburi la mtu wa Mungu ambaye alikuja kutoka Yuda na kutabiri mambo ambayo umeyafanya dhidi ya madhabahu pale Betheli.” Naye akaagiza, “Mwacheni hapo, mtu yeyote asiondoe mifupa yake.” Kwa hiyo waliiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya nabii aliyetoka Samaria. Katika kila mji wa Samaria mfalme Yosia aliharibu mahali pa kuabudia miungu ya uongo palipojengwa na wafalme wa Israeli, ili kumkashifu Mwenyezi-Mungu. Madhabahu hayo yote aliyaharibu kama vile alivyofanya huko Betheli. Aliwaua makuhani wote wa miungu ya uongo juu ya madhabahu ambapo walitumikia na kuchoma mifupa yao juu ya madhabahu hayo. Kisha alirudi Yerusalemu. Kisha mfalme aliwaamuru watu wote, akisema, “Mfanyieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, Pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano.” Hakuna Pasaka iliyosherehekewa kama hii tangu wakati wa waamuzi waliowaamua Waisraeli wala wakati wa ufalme wa Israeli au wa Yuda. Lakini, katika mwaka wa kumi na nane wa enzi ya Yosia, Pasaka ilisherehekewa kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu katika Yerusalemu. Tena, ili mfalme Yosia atekeleze sheria zote zilizoandikwa katika kitabu alichokipata kuhani mkuu Hilkia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, aliondoa katika nchi ya Yuda na Yerusalemu, wachawi, watabiri, vinyago vya miungu, sanamu za miungu pamoja na vitu vyote vya kuchukiza. Kabla ya Yosia au baada yake hakuna mfalme yeyote aliyekuwa kama yeye, ambaye alimtumikia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wake wote, kwa nguvu zake zote na kwa roho yake yote kulingana na sheria ya Mose. Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu hakuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, kwa sababu hasira yake iliwaka dhidi ya Yuda kwa ajili ya vitendo vya kukasirisha, ambavyo Manase alifanya dhidi yake. Naye Mwenyezi-Mungu alisema, “Nitawafukuza watu wa Yuda kutoka mbele yangu kama vile nilivyofanya kwa watu wa Israeli; nitaukataa mji wa Yerusalemu ambao niliuchagua niliposema, ‘Jina langu litakuwa humo.’” Matendo mengine ya Yosia na yale yote aliyofanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Wakati wa kutawala kwake, Farao Neko wa Misri alikwenda mpaka mto Eufrate ili kukutana na mfalme wa Ashuru. Naye mfalme Yosia akaondoka ili kupambana naye; lakini Farao Neko alipomwona alimuua kule Megido. Maofisa wake wakaibeba maiti yake katika gari na kuirejesha Yerusalemu walikomzika katika kaburi lake mwenyewe. Kisha watu wa Yuda wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia wakampaka mafuta na kumtawaza kuwa mfalme mahali pa baba yake. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala, akatawala kwa miezi mitatu huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Hamutali binti Yeremia wa Libna. Yehoahazi alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama babu zake walivyofanya. Ili asiendelee kutawala huko Yerusalemu, Farao Neko alimtia nguvuni huko Ribla katika nchi ya Hamathi, akaitoza nchi kodi ya kilo 3,400 za madini ya fedha na kilo 34 za dhahabu. Farao Neko akamtawaza Eliakimu mwana wa mfalme Yosia mahali pa baba yake Yosia, akabadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu. Lakini alimchukua Yehoahazi mbali mpaka Misri na kufia huko. Mfalme Yehoyakimu alimpa Farao fedha na dhahabu, lakini aliitoza nchi kodi ili aweze kutekeleza matakwa ya Farao ya kupewa fedha. Aliwatoza wananchi fedha na dhahabu. Kila mmoja alitoa kiasi alichokadiria mfalme, naye akampa Farao Neko. Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, na alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake lilikuwa Zebida binti Pedaya wa Ruma. Yehoyakimu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama waliyoyafanya babu zake wote. Nebukadneza mfalme wa Babuloni aliishambulia Yuda. Yehoyakimu, alimtumikia kwa miaka mitatu halafu aliacha kumtii, akamwasi. Basi, Mwenyezi-Mungu akampelekea makundi ya Wababuloni, Waaramu, Wamoabu na Waamoni washambulie nchi ya Yuda na kuiharibu, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu alilolisema kwa watumishi wake manabii. Hakika mambo haya yaliikumba nchi ya Yuda kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, ili kuwahamisha kutoka mbele yake, kwa sababu ya dhambi za mfalme Manase na yote aliyoyatenda, na kwa sababu ya damu isiyo na hatia aliyoimwaga. Mwenyezi-Mungu hakumsamehe makosa hayo. Basi matendo mengine ya Yehoyakimu na yote aliyoyafanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Yehoyakimu akafariki, na mwanawe Yehoyakini akatawala mahali pake. Mfalme wa Misri hakutoka tena nchini kwake, kwa sababu mfalme wa Babuloni aliitwaa na kuimiliki nchi yote iliyokuwa chini ya mfalme wa Misri hapo awali tangu kijito cha Misri mpaka mto Eufrate. Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miezi mitatu. Mama yake alikuwa Nehushta binti Elnathani, mkazi wa Yerusalemu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama aliyoyafanya baba yake. Wakati huo jeshi la Nebukadneza mfalme wa Babuloni, lilishambulia mji wa Yerusalemu na kuuzingira. Wakati majeshi yalipokuwa yanauzingira mji, Nebukadneza mwenyewe alikuja Yerusalemu, na Yehoyakini mfalme wa Yuda alijisalimisha kwa mfalme wa Babuloni, yeye mwenyewe pamoja na mama yake, watumishi wake, maofisa na maakida wake. Mfalme wa Babuloni alimchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. Vilevile, pia kama Mwenyezi-Mungu alivyosema, Nebukadneza alichukua mali yote iliyokuwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na ndani ya ikulu. Alikatakata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Solomoni mfalme wa Israeli alitengeneza. Vyombo hivyo vilikuwa ndani ya hekalu la Mwenyezi-Mungu. Alichukua watu wote wa Yerusalemu: Wakuu wote, watu wote waliokuwa mashujaa, mateka 10,000, na mafundi wote na wahunzi. Hakuna aliyebaki isipokuwa waliokuwa maskini kabisa nchini. Alimchukua Yehoyakini mpaka Babuloni pamoja na mama yake mfalme, wake za mfalme, maofisa wake na wakuu wa nchi; wote hao aliwatoa Yerusalemu, akawapeleka Babuloni. Nebukadneza alichukua watu mashujaa wa Yuda jumla yao watu 7,000 pamoja na mafundi hodari na wahunzi 1,000; wote hawa wakiwa watu wenye nguvu na wa kuweza kupigana vitani. Nebukadneza akamtawaza Matania, mjomba wake Yehoyakini, kuwa mfalme badala yake, akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala; alitawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, mkazi wa mji wa Libna. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile alivyofanya mfalme Yehoyakimu. Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia sana watu wa Yerusalemu na Yuda, hata akawafukuza mbali naye. Sedekia alimwasi mfalme wa Babuloni. Katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi wa mwaka wa tisa wa utawala wake Sedekia, Nebukadneza mfalme wa Babuloni alifika na jeshi lake, akaushambulia mji wa Yerusalemu, akauzingira na kujenga ngome kuuzunguka. Mji uliendelea kuzingirwa mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia. Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne njaa ilikuwa kali sana mjini hata hapakuwapo chakula chochote kwa ajili ya wakazi wake. Basi, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa, nao askari wote wakakimbia wakati wa usiku wakipitia katika bustani ya mfalme kwenye lango katikati ya kuta mbili, wakaenda upande wa Araba, ingawa Wababuloni walikuwa wameuzunguka mji. Lakini jeshi la Wakaldayo lilimfuatia mfalme na kumteka kwenye tambarare za Yeriko, nao askari wake wote walimwacha, wakatawanyika. Basi, Wakaldayo walimteka mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla, naye akamhukumu. Halafu waliwaua wanawe akiona kwa macho yake mwenyewe, kisha wakamngoa macho yake. Mwishowe walimfunga kwa pingu, wakampeleka Babuloni. Katika siku ya saba ya mwezi wa tano wa mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliingia Yerusalemu. Aliichoma moto nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu na nyumba zote za Yerusalemu; kila nyumba kubwa aliichoma moto. Nao askari wote wa Wakaldayo waliokuwa pamoja na kapteni na walinzi wa mfalme walizibomoa kuta zilizouzunguka mji wa Yerusalemu. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebakia mjini na wale wote waliokuwa wamejisalimisha kwa mfalme wa Babuloni pamoja na watu wengine wote. Lakini aliacha baadhi ya watu waliokuwa maskini kabisa nchini. Aliwaacha watunze mizabibu na kulima mashamba. Wakaldayo walivunja vipandevipande nguzo za shaba ambazo zilikuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, pamoja na vikalio vyake, birika kubwa la shaba nyeusi lililokuwamo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaichukua shaba nyeusi mpaka Babuloni. Vilevile walichukua vyungu, masepetu, makasi na miiko iliyotumiwa kuchomea ubani na vyombo vingine vyote vya shaba nyeusi vilivyotumiwa katika huduma ya hekalu, wakachukua na vyetezo na mabakuli. Kapteni wa walinzi wa mfalme alipeleka mbali kila chombo cha dhahabu na kila chombo cha fedha. Shaba yote nyeusi aliyotumia Solomoni kutengeneza zile nguzo mbili, birika lile kubwa na vikalio kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu haikuweza kupimwa kwa uzito. Kila nguzo ilikuwa na urefu wa mita 8, na juu yake kulikuwa na kichwa cha shaba nyeusi, urefu wa kila kichwa ulikuwa mita 1.25. Kila kichwa kilizungushiwa mapambo ya makomamanga, yote ya shaba nyeusi. Kisha Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme alimchukua mateka Seraya kuhani mkuu, Sefania kuhani wa pili pamoja na maofisa walinda milango watatu; alimchukua towashi mmoja huko mjini ambaye alikuwa akiwaongoza askari vitani, pamoja na watu watano mashuhuri wa mfalme ambao aliwakuta huko. Vilevile, alimchukua katibu wa kamanda mkuu wa jeshi ambaye alitunza kumbukumbu za jeshi pamoja na watu sitini mashuhuri ambao aliwakuta mjini Yerusalemu. Nebuzaradani kapteni wa walinzi aliwachukua watu hao, akawapeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliwapiga na kuwaua watu hao huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Hivyo watu wa Yuda walichukuliwa mateka nje ya nchi yao. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni alimteua Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, kuwa mtawala wa watu wote wa Yuda ambao hawakupelekwa Babuloni. Kisha makapteni wote wa majeshi pamoja na watu wao waliposikia kuwa mfalme wa Babuloni alimteua Gedalia kuwa mtawala, walimwendea Gedalia huko Mizpa. Watu hao walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani mwana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka. Naye Gedalia aliapa mbele yao na watu wao, akasema, “Msiogope kwa sababu ya maofisa wa Wakaldayo. Kaeni nchini mumtumikie mfalme wa Babuloni na mambo yote yatawaendea vema.” Mnamo mwezi wa saba, Ishmaeli mwana wa Nethania, mjukuu wa Elishama aliyekuwa wa ukoo wa kifalme, alifika kwa Gedalia akiandamana na watu kumi, akamshambulia Gedalia, akamuua. Vilevile, aliwaua Wayahudi na Wakaldayo waliokuwa naye. Halafu, Waisraeli wote, wadogo kwa wakubwa pamoja na maofisa wa majeshi, waliondoka, wakaenda Misri, kwa sababu waliwaogopa Wakaldayo. Mnamo mwaka wa thelathini na mbili, Evil-merodaki mfalme wa Babuloni, alipoanza kutawala, mwaka huohuo alimsamehe Yehoyakini mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani. Hiyo ilikuwa siku ya ishirini na saba ya mwezi wa kumi na mbili, mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini alipochukuliwa mateka. Aliongea naye vizuri na kumpa nafasi ya heshima kuliko wafalme wengine waliokuwa pamoja naye huko Babuloni. Basi, Yehoyakini alibadili mavazi yake ya kifungoni. Kila siku alikuwa anapata daima chakula chake kwa mfalme. Alipatiwa na mfalme mahitaji yake siku kwa siku, maisha yake yote. Adamu alimzaa Sethi, Sethi akamzaa Enoshi, Enoshi akamzaa Kenani, Kenani akamzaa Mahalaleli, Mahalaleli akamzaa Yaredi, Yaredi akamzaa Henoki, Henoki akamzaa Methusela. Methusela alimzaa Lameki, Lameki akamzaa Noa. Noa alikuwa na wana watatu: Shemu, Hamu na Yafethi. Wana wa Yafethi walikuwa Gomeri, Magogu, Madai, Yavani, Tubali, Mesheki na Tirasi. Wana wa Gomeri walikuwa Ashkenazi, Difathi na Togama. Wana wa Yavani walikuwa Elisha, Tarshishi, Kitimu na Rodanimu. Wana wa Hamu walikuwa Kushi, Misri, Puti na Kanaani. Wana wa Kushi walikuwa Seba, Havila, Sabta, Raama na Sabteka. Wana wa Raama walikuwa Sheba na Dedani. Kushi alimzaa Nimrodi, aliyekuwa mtu shujaa wa kwanza duniani. Wazawa wa Misri ni Waludi, Waanamu, Walehabi, Wanaftuhi, Wapathrusi Wakaftori na Wakasluhi (hao ndio asili ya Wafilisti). Wana wa Kanaani walikuwa Sidoni, mzaliwa wake wa kwanza, na Hethi. Kanaani pia ndiye babu yao Wayebusi, Waamori, Wagirgashi, Wahivi, Waarki, Wasini, Waarvadi, Wasemari na Wahamathi. Wana wa Shemu walikuwa Elamu, Ashuri, Arpaksadi, Ludi, Aramu, Usi, Huli, Getheri na Mesheki. Arpaksadi alimzaa Shela, Shela akamzaa Eberi. Eberi alikuwa na wana wawili; mmoja wao aliitwa Pelegi, (kwa maana wakati wake watu walikuwa wametawanyika duniani), na ndugu yake aliitwa Yoktani. Wana wa Yoktani walikuwa Almodadi, Shelefu, Hasarmawethi, Yera, Hadoramu, Uzali, Dikla, Obali, Abimaeli, Sheba, Ofiri, Havila na Yobabu. Hao watu ni wana wa Yoktani. Ukoo wa Abrahamu kutokea Shemu ni kama ifuatavyo: Shemu alimzaa Arpaksadi, naye Arpaksadi akamzaa Shela. Shela akamzaa Eberi, Eberi akamzaa Pelegi, Pelegi akamzaa Reu; Reu akamzaa Serugi, Serugi akamzaa Nahori, Nahori akamzaa Tera, na Tera akamzaa Abramu, ambaye ndiye Abrahamu. Abrahamu alikuwa na watoto wawili wa kiume: Isaka na Ishmaeli. Hivi ndivyo vizazi vyao: Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli alikuwa Nebayothi na wengine ni Kedari, Adbeeli, Mibsamu, Mishma, Duma, Masa, Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi na Kedema. Hao ndio wana wa Ishmaeli. Abrahamu alikuwa na suria aliyeitwa Ketura. Ketura alimzalia Abrahamu: Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua. Wana wa Yokshani walikuwa Sheba na Dedani. Wana wa Midiani walikuwa: Efa, Eferi, Henoki, Abida na Eldaa. Wote hao walikuwa wazawa wa Ketura. Isaka, mwana wa Abrahamu, alikuwa na wana wawili: Esau na Israeli. Wana wa Esau walikuwa Elifazi, Reueli, Yeushi, Yalamu na Kora. Wana wa Elifazi walikuwa Temani, Omari, Sefo, Gatamu, Kenazi, Timna na Amaleki. Wana wa Reueli walikuwa Nahathi, Zera, Shama na Miza. Wana wa Seiri walikuwa Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana, Dishoni, Eseri na Dishani. Wana wa Lotani walikuwa wawili: Hori na Homamu. Lotani alikuwa na dada yake aliyeitwa Timna. Wana wa Shobali walikuwa Alvani, Manahathi, Ebali, Shefi na Onamu. Wana wa Sibeoni walikuwa Aya na Ana. Mwana wa Ana alikuwa Dishoni; na wana wa Dishoni walikuwa Hamrani, Eshbani, Ithrani na Kerani. Wana wa Eseri walikuwa Bilhani, Zaawani na Akani; na wana wa Dishoni walikuwa Usi na Arani. Wafuatao ndio wafalme waliotawala nchi ya Edomu kabla mfalme yeyote hajatawala Waisraeli: Bela mwana wa Beori alitawala nchi ya Edomu, akiwa na makao yake makuu katika mji wa Dinhaba. Bela alipofariki, Yobabu mwana wa Zera kutoka Bosra alitawala badala yake. Yobabu alipofariki, Hushamu wa nchi ya Watemi alitawala badala yake. Hushamu alipofariki, Hadadi mwana wa Bedadi alitawala badala yake, makao yake makuu yakiwa katika mji wa Avithi. Huyu ndiye aliyewapiga na kuwashinda Wamidiani katika nchi ya Moabu. Hadadi alipofariki, Samla kutoka Masreka alitawala badala yake. Samla alipofariki, Shauli kutoka Rehobothi ulio karibu na mto Eufrate, alitawala badala yake. Shauli alipofariki, Baal-hanani mwana wa Akbori alitawala badala yake. Baal-hanani alipofariki, Hadadi kutoka Pai alitawala badala yake na jina la mkewe Akbori lilikuwa Mehetabeli, binti Matredi, binti Mezahabu. Naye Hadadi akafariki. Wakuu wa makabila ya Edomu walikuwa Timna, Alva, Yethethi, Oholibama, Ela, Pinoni, Kenazi, Temani, Mibsari, Magdieli na Iramu. Hao ndio wakuu wa makabila ya Edomu. Israeli alikuwa na wana wa kiume kumi na wawili: Reubeni, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Zebuluni, Dani, Yosefu, Benyamini, Naftali, Gadi na Asheri. Wana wa Yuda waliozaliwa na Bethshua, mkewe Mkanaani, walikuwa Eri, Onani na Shela. Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, basi Mwenyezi-Mungu akamuua. Na Tamari, mkwewe, alimzalia wana wawili: Peresi na Zera. Jumla, wana wa Yuda walikuwa watano. Peresi alikuwa na wana wawili: Hesroni na Hamuli. Zera nduguye alikuwa na wana watano: Zimri, Etheni, Hemani, Kalkoli na Dara. Mwana wa Karmi, alikuwa Akari. Huyu aliwaletea Waisraeli taabu kwa sababu alijiwekea nyara zilizokuwa zimewekwa wakfu. Ethani alikuwa na mwana mmoja, jina lake Azaria. Wana wa Hesroni walikuwa Yerameeli, Ramu na Kelubai. Ramu alimzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nashoni, mkuu wa kabila la Yuda. Nashoni alimzaa Salma, Salma akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obedi, Obedi akamzaa Yese. Yese aliwazaa Eliabu, mwanawe wa kwanza, wa pili Abinadabu, wa tatu Shimea, wa nne Nethaneli, wa tano Radai, wa sita Osemu na wa saba Daudi. Dada zao walikuwa Seruya na Abigaili. Wana wa Seruya walikuwa watatu: Abishai, Yoabu na Asaheli. Abigaili alimzaa Amasa ambaye baba yake alikuwa Yetheri, Mwishmaeli. Kalebu, mwana wa Hesroni, kutokana na wake zake wawili, Azuba na Yeriothi, aliwazaa Yesheri, Shaobabu na Ardoni. Azuba alipofariki, Kalebu alimwoa Efratha aliyemzalia Huri. Huri alimzaa Uri, naye Uri akamzaa Besaleli. Hesroni alipokuwa na umri wa miaka sitini, alimwoa binti Makiri, dada yake Gileadi. Huyo alimzalia mwana jina lake Segubu. Segubu alimzaa Yairi ambaye alitawala miji mikubwa ishirini na mitatu katika nchi ya Gileadi. Lakini falme za Geshuri na Aramu ziliwashambulia na kuwanyanganya miji ya Haroth-yairi, Kenathi na vijiji vyake, jumla miji sitini. Hao wote walikuwa wazawa wa Makiri, baba yake Gileadi. Baada ya Hesroni kufariki, Kalebu alimwoa Efratha, mjane wa Hesroni, baba yake. Efratha alimzalia Kalebu mwana jina lake Ashuri, aliyekuwa mwanzilishi wa mji wa Tekoa. Yerameeli, mzaliwa wa kwanza wa Hesroni, alikuwa na wana watano: Ramu, mzaliwa wake wa kwanza, Buna, Oreni, Osemu na Ahiya. Yerameeli alikuwa na mke mwingine jina lake Atara. Huyu alimzalia Yerameeli mwana, jina lake Onamu. Wana wa Ramu, mzaliwa wa kwanza wa Yerameeli, walikuwa Maasi, Yamini na Ekeri. Wana wa Onamu walikuwa Shamai na Yada. Nao wana wa Shamai walikuwa Nadabu na Abishuri. Abishuri alioa mke, jina lake Abihaili, naye akamzalia wana wawili: Abani na Molidi. Wana wa Nadabu walikuwa Seledi na Apaimu; lakini Seledi alifariki bila watoto. Apaimu alikuwa na mwana mmoja aliyeitwa Ishi. Ishi alimzaa Sheshani, na Sheshani akamzaa Alai. Yada, nduguye Shamai, alikuwa na wana wawili: Yetheri na Yonathani. Lakini Yetheri alifariki bila watoto. Yonathani alikuwa na wana wawili: Pelethi na Zaza. Wote hao ni wazawa wa Yerameeli. Sheshani hakuwa na watoto wa kiume; alikuwa na binti tu. Hata hivyo, alikuwa na mtumwa wa Kimisri, jina lake Yarha. Hivyo, Sheshani akamwoza Yarha mtumwa wake, mmoja wa binti zake, naye akamzalia mwana jina lake Atai. Atai alimzaa Nathani, Nathani akamzaa Zabadi. Zabadi akamzaa Eflali, Eflali akamzaa Obedi, Obedi akamzaa Yehu, Yehu akamzaa Azaria, Azaria akamzaa Helesi, Helesi akamzaa Eleasa, Eleasa akamzaa Sismai, Sismai akamzaa Shalumu, Shalumu akamzaa Yekamia, na Yekamia akamzaa Elishama. Mzaliwa wa kwanza wa Kalebu, nduguye Yerameeli, aliitwa Mesha. Mesha alimzaa Zifu, Zifu akamzaa Maresha, Maresha akamzaa Hebroni. Hebroni alikuwa na wana wanne: Kora, Tapua, Rekemu na Shema. Shema alikuwa baba yake Rahamu na babu yake Rekemu. Rekemu nduguye Shema alimzaa Shamai, Shamai akamzaa Maoni, na Maoni akamzaa Beth-suri. Kalebu alikuwa na suria, jina lake Efa. Huyu alimzalia wana wengine watatu: Harani, Mosa na Gazezi. Harani alimzaa Gazezi. Yadai alikuwa na wana sita: Regemu, Yothamu, Geshani, Peleti, Efa na Shaafu. Kalebu alikuwa na suria mwingine jina lake Maaka. Huyu alimzalia wana wawili: Sheberi na Tirhana. Maaka alimzalia Kalebu wana; Shaafu mwanzilishi wa mji wa Madmana, na Sheva, mwanzilishi wa mji wa Makbena na Gibea. Kalebu alikuwa pia na binti, jina lake Aksa. Kalebu alikuwa na wazawa wengine pia kwa mkewe Efratha. Huri, mzaliwa wake wa kwanza, alikuwa na wana watatu: Shobali, mwanzilishi wa mji wa Kiriath-yearimu, wa pili Salma, mwanzilishi wa mji wa Bethlehemu, na wa tatu Herefu, mwanzilishi wa mji wa Bethi-gaderi. Shobali, mwanzilishi wa mji wa Kiriath-yearimu, alikuwa pia babu yao watu wa Haroe, na nusu ya wakazi wa mji wa Menuhothi, pamoja na koo zifuatazo zilizoishi Kiriath-yearimu: Waithri, Waputhi, Washumathi na Wamishrai. (Wasorathi na Waeshtaoli walitokana na watu hao). Salma, mwanzilishi wa mji wa Bethlehemu alikuwa babu ya Wanetofathi, Waatroth-beth-yoabu na nusu ya Wamenahathi yaani Wasori. Jamaa zifuatazo za waandishi ziliishi katika mji wa Yabesi: Watirathi, Washimeathi na Wasukathi. Wao ndio Wakeni waliotoka katika uzao wa Hamathi, aliyekuwa babu yao waliokuwa wa ukoo wa Warekabu. Hawa ndio wana wa mfalme Daudi waliozaliwa wakati alipokuwa huko Hebroni: Amnoni, mzaliwa wake wa kwanza; mama yake aliitwa Ahinoamu, Myezreeli; wa pili Danieli ambaye mama yake alikuwa Abigaili, Mkarmeli; wa tatu alikuwa Absalomu, ambaye mama yake alikuwa Maaka, bintiye Talmai mfalme wa Geshuri; wa nne alikuwa Adoniya, ambaye mama yake alikuwa Hagithi; wa tano alikuwa Shefatia, ambaye mama yake alikuwa Abitali; na wa sita alikuwa Ithreamu, ambaye mama yake alikuwa Egla. Wote sita, walizaliwa Hebroni ambako Daudi alitawala kwa muda wa miaka saba na nusu. Huko Yerusalemu, alitawala kwa muda wa miaka thelathini na mitatu. Wafuatao ni wana wa mfalme Daudi alipokuwa Yerusalemu: Mkewe Bathshua, bintiye Amieli, alimzalia wana wanne: Himea, Shobabu, Nathani na Solomoni. Na mbali na hao alikuwa na wana wengine tisa: Ibhari, Elishua, Elifaleti, Noga, Nefegi, Yafia, Elishama, Eliada na Elifeleti. Hao wote walikuwa wana wa Daudi, mbali na wale wengine waliozaliwa na masuria wake. Daudi alikuwa na binti pia, aliyeitwa Tamari. Wazawa wa mfalme Solomoni: Solomoni alimzaa Rehoboamu, aliyemzaa Abiya, aliyemzaa Asa, aliyemzaa Yehoshafati, aliyemzaa Yehoramu, aliyemzaa Ahazia, aliyemzaa Yoashi, aliyemzaa Amazia, aliyemzaa Uzia, aliyemzaa Yothamu, aliyemzaa Ahazi, aliyemzaa Hezekia, aliyemzaa Manase, aliyemzaa Amoni, aliyemzaa Yosia. Yosia alikuwa na wana wanne: Yohanani, mzaliwa wake wa kwanza, wa pili Yehoyakimu, wa tatu Sedekia na wa nne Shalumu. Yehoyakimu alikuwa na wana wawili: Yekonia na Sedekia. Wana wa Yekonia aliyechukuliwa mateka na Wababuloni walikuwa saba: Shealtieli, Malkiramu, Pedaya, Shenazari, Yekamia, Hoshama na Nedabia. Wana wa Pedaya walikuwa Zerubabeli na Shimei. Zerubabeli alikuwa na wana wawili: Meshulamu na Hanania, na binti mmoja, jina lake Shelomithi. Zerubabeli pia alikuwa na wana wengine watano: Hashuba, Oheli, Berekia, Hasadia na Yushab-hesedi. Wana wa Hanania walikuwa Pelatia na Yeshaya. Yeshaya alimzaa Refaya, aliyemzaa Arnani, aliyemzaa Obadia, aliyemzaa Shekania. Shekania alimzaa Shemaya. Wana wa Shemaya walikuwa sita: Hatushi, Igali, Baria, Nearia na Shafati. Nearia alikuwa na wana watatu: Eliehonai, Hizkia na Azrikamu. Eliehonai alikuwa na wana saba: Hodavia, Eliashibu, Pelaya, Akubu, Yohanani, Delaya na Anani. Wana wa Yuda walikuwa Peresi, Hesroni, Karmi, Huri na Shobali. Reaya, mwana wa Shobali, alimzaa Yahathi, aliyekuwa baba yake Ahumai na Lahadi, hizo ndizo jamaa za Wasorathi. Wana wa Etamu walikuwa Yezreeli, Ishma na Idbashi. Walikuwa na dada mmoja aliyeitwa Haselelponi. Penueli aliwazaa Gedori na Ezeri, na Ezeri akamzaa Husha. Hao ndio wazawa wa Huri mzaliwa wa kwanza wa Efratha, baba yake Bethlehemu. Ashuru, mwanzilishi wa mji wa Tekoa, alikuwa na wake wawili: Hela na Naara. Naara alimzalia wana wanne: Ahuzamu, Heferi, Temeni na Haahashtari. Hela alimzalia wana watatu: Serethi, Ishari na Ethnani. Hakosi aliwazaa Anubi na Sobeba, na ndiye aliyekuwa baba wa jamaa za wazawa wa Aharheli, mwana wa Harumu. Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yabesi, aliyeheshimiwa kuliko ndugu zake wote. Mama yake alimpa jina la Yabesi kwa sababu alimzaa kwa maumivu. Lakini Yabesi alimwomba Mungu wa Israeli akisema, “Ee Mungu, nakusihi unibariki na kuipanua mipaka yangu. Mkono wako uwe pamoja nami na unilinde kutokana na jambo lolote ovu, lisiniumize.” Naye Mungu akamjalia yale aliyoomba. Kelubu, nduguye Shuha, alimzaa Mehiri na Mehiri akamzaa Eshtoni. Eshtoni alikuwa na wana watatu: Beth-rafa, Pasea na Tehina. Tehina alikuwa mwanzilishi wa mji wa Ir-nahashi. Wazawa wa watu hawa waliishi Reka. Wana wa Kenazi walikuwa: Othnieli na Seraya; na wana wa Othnieli walikuwa Hathathi na Meonothai. Meonothai alimzaa Ofra. Seraya alimzaa Yoabu, mwanzilishi wa Bonde la Mafundi, lililopewa jina hilo kwa sababu wote waliokuwa humo walikuwa mafundi stadi. Kalebu mwana wa Yefune alikuwa na wana watatu: Iru, Ela na Naamu. Na mwana wa Ela alikuwa Kenazi. Wana wa Yehaleli walikuwa Zifu, Zifa, Tiria na Asareli. Wana wa Ezra walikuwa Yetheri, Meredi, Eferi na Yaloni. Meredi alimwoa Bithia, bintiye Farao, na hawa ndio wana aliomzalia Meredi: Miriamu, Shamai na Ishba, mwanzilishi wa mji wa Eshtemoa. Meredi alikuwa na mke mwingine Myahudi. Huyu alimzalia Yeredi, mwanzilishi wa Mji wa Gedori, Heberi, mwanzilishi wa mji wa Soko, na Yekuthieli, mwanzilishi wa Mji wa Zanoa. Hodia alimwoa dada yake Nahamu ambaye wazawa wake ndio waanzilishi wa kabila la Garmi, lililoishi katika mji wa Keila, na kabila la Maakathi, lililoishi katika mji wa Eshtemoa. Wana wa Shimoni walikuwa Amnoni, Rina, Ben-hanani na Tiloni. Ishi alikuwa na wana wawili: Zohethi na Ben-zohethi. Wana wa Shela, mwana wa Yuda, walikuwa Eri, mwanzilishi wa mji wa Leka, Laada, mwanzilishi wa mji Maresha; ukoo wa wafuma nguo za kitani waliokuwa wakiishi katika mji wa Beth-ashbea; Yokimu na watu walioishi katika mji wa Kozeba; na Yoashi na Sarafi waliotawala huko Moabu na wakarejea Lehemu. (Taarifa hizi ni za zamani sana.) Hawa ndio wafinyanzi walioishi katika miji ya Netaimu na Gedera, wakimhudumia mfalme. Simeoni alikuwa na wana watano: Nemueli, Yamini, Yaribu, Zera na Shauli. Mwana wa Shauli alikuwa Shalumu; Shalumu alimzaa Mibsamu na Mibsamu akamzaa Mishma. Mishma alimzaa Hamueli, aliyemzaa Zakuri, na Zakuri akamzaa Shimei. Shimei alikuwa na wana kumi na sita na binti sita, lakini ndugu zake hawakuwa na wana wengi, na jamii yake pia haikuongezeka kama kabila la Yuda. Miji walimokuwa wakiishi ilikuwa Beer-sheba, Molada, Hasar-shuali, Bilha, Ezemu, Toladi; Bethueli, Horma, Siklagi, Beth-markabothi, Hazar-susimu, Beth-biri na Shaaraimu. Hiyo ndiyo miji yao mpaka wakati wa utawala wa mfalme Daudi. Pia, waliishi katika miji mingine mitano: Etamu, Aini, Rimoni, Tokeni na Ashani, pamoja na vijiji kandokando ya miji hiyo huko Baali. Hayo ndiyo yaliyokuwa makao yao, nao waliweka kumbukumbu ya nasaba yao. Watu wafuatao walikuwa wakuu wa koo zao: Meshobabu, Yamleki, Yosha mwana wa Amazia, Yoeli, Yehu (mwana wa Yoshibia, mwana wa Seraya, mwana wa Asieli.) Eliehonai, Yaakoba, Yeshohaya, Asaya, Adieli, Yesimieli, Benaya, Ziza (mwana wa Shifi, mwana wa Aloni, mwana wa Yedaya, mwana wa Shimri na mwana wa Shemaya). Jamaa zao waliendelea kuongezeka kwa wingi sana. Hawa waliotajwa majina ni wakuu katika jamaa zao na koo zao ziliongezeka sana. Walienea hadi kwenye lango la mji wa Gedori, upande wa mashariki wa bonde, ili kuwatafutia kondoo wao malisho. Hapo, walipata malisho tele, tena mazuri sana na pia nchi ilikuwa wazi, tulivu na yenye amani, kwani wenyeji wa nchi hiyo wa hapo awali walikuwa Wahamu. Katika siku za mfalme Hezekia wa Yuda, watu hao waliotajwa majina yao walikwenda huko Gedori, wakaharibu hema za Wameuni waliokuwa wakiishi huko na kuwafukuza kabisa mpaka leo. Walifanya makao yao ya kudumu huko kwa sababu kulikuwa na malisho tele kwa ajili ya kondoo wao. Watu wengine wa kabila la Simeoni wapatao 500 walikwenda mpaka kwenye mlima Seiri. Waliongozwa na Pelatia, Nearia, Refaya na Uzieli, wana wa Ishi. Hapo waliwaua Waamaleki waliosalia baada ya kunusurika, na wakaishi huko mpaka leo. Hawa ndio wazawa wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli. (Ingawa Reubeni alikuwa mzaliwa wa kwanza haki yake ya mzaliwa wa kwanza ilipewa Yosefu nduguye kwa sababu Reubeni alilala na suria wa baba yake. Hivyo, yeye hakutiwa katika orodha ya ukoo kulingana na haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Ingawa kabila la Yuda ndilo lililokuja kuwa lenye nguvu zaidi kuliko mengine, na watawala walitoka humo, haki ya mzaliwa wa kwanza ilikuwa ya Yosefu). Wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli, walikuwa Henoki, Palu, Hesroni na Karmi. Wazawa wa Yoeli toka kizazi hadi kizazi walikuwa Shemaya, Gogi, Shimei, Mika, Reaya, Baali, na Beera, ambaye mfalme Tiglath-pileseri wa Ashuru, alimchukua mateka ingawa alikuwa kiongozi wa Wareubeni, akampeleka uhamishoni. Wakuu wa koo wafuatao waliandikishwa katika orodha ya kumbukumbu ya kabila la Reubeni, Yeieli, Zekaria, Bela, mwana wa Azazi na mjukuu wa Shema, wa ukoo wa Yoeli, uliokuwa ukiishi Aroeri na katika eneo lote la kaskazini hadi Bela na Baal-meoni. Pia, kwa maana mifugo yao iliongezeka kwa wingi sana, walisambaa upande wa mashariki hadi kwenye maingilio ya jangwa lililoenea hadi mto Eufrate. Katika siku za mfalme Shauli, kabila la Reubeni lilizusha vita dhidi ya Wahajiri, wakawaua vitani na kuitwaa ardhi yao yote mashariki mwa Gileadi, wakaishi humo. Kabila la Gadi lilipakana na kabila la Reubeni upande wa kaskazini, katika nchi ya Bashani iliyoenea mashariki hadi Saleka. Yoeli ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa ukoo ulioongoza, wa pili Shafamu. Yanai na Shefati walikuwa waanzilishi wa koo nyingine huko Bashani. Ndugu zao kulingana na koo zao walikuwa saba: Mikaeli, Meshulamu, Sheba, Yorai, Yaakani, Zia na Eberi. Wote hawa walikuwa wana wa Abihaili, aliyekuwa mwana wa Huri, mwana wa Yaroa, mwana wa Yeshishai, mwana wa Yado, mwana wa Buzi. Ahi, aliyekuwa mwana wa Abdieli na mjukuu wa Guni, alikuwa mkuu katika koo hizi. Waliishi katika sehemu ya Gileadi, katika Bashani na miji yake na katika malisho yote ya Sharoni, hadi mipakani. Watu hao wote waliandikishwa katika koo, katika siku za Yothamu, mfalme wa Yuda, na Yeroboamu, mfalme wa Israeli. Makabila ya Reubeni, Gadi na Manase ya mashariki, yalikuwa na wanajeshi shupavu wapatao 44,760, wenye ngao na mapanga, wavuta pinde stadi vitani. Walipigana vita na makabila ya Wahajiri, Yeturi, Nafishi na Nodabu. Waliweka tumaini lao kwa Mungu na wakamwomba awasaidie, naye akaitikia ombi lao na kuwatia mikononi mwao Wahajiri pamoja na marafiki zao. Waliteka nyara ngamia 50,000, kondoo 250,000, punda 2,000 na mateka hai 100,000. Waliua maadui wengi sana kwa sababu vita hivyo vilikuwa ni vita vya Mungu. Nao waliendelea kuishi katika nchi hiyo, mpaka wakati wa uhamisho. Watu wa Manase ya mashariki waliishi katika nchi ya Bashani. Idadi yao iliongezeka kwa wingi sana, wakasambaa upande wa kaskazini hadi Baal-hermoni, Seniri na mlima Hermoni. Wafuatao ndio waliokuwa wakuu wa koo za kabila hilo: Eferi, Ishi, Elieli, Azrieli, Yeremia, Hodavia na Yadieli. Wote walikuwa askari shujaa, watu mashuhuri sana na viongozi katika koo hizo. Lakini watu walimwasi Mungu wa babu zao, wakafanya uzinzi kwa kuabudu miungu ya wakazi wa nchi hizo ambazo Mungu aliziangamiza mbele yao. Basi, Mungu wa Israeli akamfanya Pulu, mfalme wa Ashuru, (ambaye pia alijulikana kama Tiglath-pileseri), aivamie nchi yao na kuwachukua mateka hao Wareubeni, Wagadi na nusu Manase ya mashariki mpaka uhamishoni huko Hala, Habori na Hara, kando ya mto Gozani, ambako wamekaa mpaka leo. Lawi alikuwa na wana watatu: Gershomu, Kohathi na Merari. Kohathi alikuwa na wana wanne: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli. Amramu alikuwa na wana wawili: Aroni na Mose, na binti mmoja jina lake Miriamu. Aroni alikuwa na wana wanne: Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari. Eleazari alimzaa Finehasi, Finehasi akamzaa Abishua, Abishua akamzaa Buki, Buki akamzaa Uzi, Uzi akamzaa Zerahia, Zerahia akamzaa Merayothi, Merayothi akamzaa Amaria, Amaria akamzaa Ahitubu, Ahitubu akamzaa Sadoki, Sadoki akamzaa Ahimaasi, Ahimaasi akamzaa Azaria, Azaria akamzaa Yohanani, na Yohanani akamzaa Azaria. (Azaria ndiye aliyefanya kazi ya ukuhani katika hekalu alilojenga mfalme Solomoni huko Yerusalemu). Azaria alimzaa Amaria, Amaria alimzaa Ahitubu, Ahitubu alimzaa Sadoki, Sadoki alimzaa Meshulamu, Meshulamu alimzaa Hilkia, Hilkia alimzaa Azaria, Azaria alimzaa Seraya, Seraya alimzaa Yehosadaki; Yehosadaki alikwenda uhamishoni wakati Mwenyezi-Mungu alipowapeleka uhamishoni watu wa Yuda na Yerusalemu kwa kuutumia mkono wa mfalme Nebukadneza. Lawi alikuwa na wana watatu: Gershomu, Kohathi na Merari. Kila mmoja wao pia alikuwa na wana. Gershomu aliwazaa Libni na Shimei; Kohathi aliwazaa Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli; naye Merari aliwazaa Mahli na Mushi. Hizi ndizo jamaa za Walawi kulingana na koo zao. Wafuatao ndio wazawa wa Gershomu kutoka kizazi hadi kizazi: Gershomu alimzaa Libni, Libni akamzaa Yahathi, Yahathi akamzaa Zima, Zima akamzaa Yoa, Yoa akamzaa Ido, Ido akamzaa Zera, Zera akamzaa Yeatherai. Hawa ndio wazawa wa Kohathi kutoka kizazi hadi kizazi: Kohathi alimzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Kora, Kora akamzaa Asiri, Asiri akamzaa Elkana, Elkana akamzaa Ebiasafu, Ebiasafu akamzaa Asiri, Asiri akamzaa Tahathi, Tahathi akamzaa Urieli, Urieli akamzaa Usia, Usia akamzaa Shauli. Wana wa Elkana walikuwa wawili: Amasai na Ahimothi. Na hawa ndio wazawa wa Ahimothi: Ahimothi alimzaa Elkana, Elkana akamzaa Sofai, Sofai akamzaa Nahathi, Nahathi akamzaa Eliabu, Eliabu akamzaa Yerohamu, Yerohamu akamzaa Elkana. Wana wa Samueli walikuwa wawili: Yoeli, mzaliwa wake wa kwanza, na Abiya, mdogo wake. Na hawa ndio wazawa wa Merari kutoka kizazi hadi kizazi: Merari alimzaa Mali, Mali akamzaa Libni, Libni akamzaa Shimei, Shimei akamzaa Uza, Uza akamzaa Shimea, Shimea akamzaa Hagia, Hagia akamzaa Asaya. Hawa ndio watu ambao mfalme Daudi aliwaweka wahudumu kama waimbaji katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, baada ya sanduku la agano kuwekwa ndani. Walifanya kazi yao ya kuimba mbele ya hema takatifu la mkutano hadi wakati mfalme Solomoni alipojenga hekalu la Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu. Waliutekeleza wajibu wao barabara, kwa zamu. Zifuatazo ni koo za wale ambao walitoa huduma hizo: Ukoo wa Kohathi: Hemani, kiongozi wa kundi la kwanza la waimbaji, alikuwa mwana wa Yoeli. Ukoo wake kutokana na Israeli ni kama ifuatavyo: Hemani, mwana wa Yoeli, mwana wa Samueli, mwana wa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elieli, mwana wa Toa, mwana wa Zufu, mwana wa Elkana, mwana wa Mahathi, mwana wa Amasai, mwana wa Elkana, mwana wa Yoeli, mwana wa Azaria, mwana wa Sefania, mwana wa Tahathi, mwana wa Asiri, mwana wa Ebiasafu, mwana wa Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, mwana wa Israeli. Asafu, ndugu yake alikuwa upande wake wa kulia. Ukoo wake kutokana na Lawi: Asafu, mwana wa Berekia, mwana wa Shimea, mwana wa Mikaeli, mwana wa Baaseya, mwana wa Malkiya, mwana wa Ethni, mwana wa Zera, mwana wa Adaya, mwana wa Ethani, mwana wa Zima, mwana wa Shimei, mwana wa Yahathi, mwana wa Gershomu, mwana wa Lawi. Ethani wa ukoo wa Merari, alikuwa kiongozi wa kundi la tatu la waimbaji. Ukoo wake kutokana na Lawi ni kama ifuatavyo: Ethani, mwana wa Kishi, mwana wa Abdi, mwana wa Maluki, mwana wa Hashabia, mwana wa Amazia, mwana wa Hilkia, mwana wa Amsi, mwana wa Bani, mwana wa Shemeri, mwana wa Mahli, mwana wa Mushi, mwana wa Merari, mwana wa Lawi. Ndugu zao wengine walipewa wajibu wa kuhudumia hema takatifu la nyumba ya Mungu. Aroni na wazawa wake ndio waliokuwa wakitoa tambiko juu ya madhabahu ya tambiko za kuteketezwa na pia juu ya madhabahu ya kufukizia ubani. Walifanya kazi zote zilizohusika na mahali patakatifu sana ili kuifanyia Israeli upatanisho. Haya yote waliyafanya kulingana na maagizo aliyotoa Mose, mtumishi wa Mungu. Wafuatao ndio wazawa wa Aroni: Aroni alimzaa Eleazari, Eleazari akamzaa Finehasi, Finehasi akamzaa Abishua, Abishua akamzaa Buki, Buki akamzaa Uzi, Uzi akamzaa Serahia, Serahia akamzaa Merayothi, Merayothi akamzaa Amaria, Amaria akamzaa Ahitubu, Ahitubu akamzaa Sadoki, Sadoki akamzaa Ahimaasi. Yafuatayo ndiyo makazi yao kulingana na mipaka yake: Wazawa wa Aroni katika jamaa ya Wakohathi kulingana na kura yao, hao walipewa mji wa Hebroni katika nchi ya Yuda na malisho kandokando yake. Lakini mashamba ya mjini pamoja na malisho yake alipewa Kalebu mwana wa Yefune. Wazawa wa Aroni walipewa miji ya makimbilio: Hebroni, Libna pamoja na malisho yake, Yatiri na Eshtemoa pamoja na malisho yake, Hileni na Debiri pamoja na malisho yake, Ashani na Beth-shemeshi pamoja na malisho yake. Katika eneo la kabila la Benyamini walipewa miji ya Geba, Alemethi na Anathothi pamoja na malisho ya miji hiyo. Miji yote waliyopewa kulingana na jamaa zao ilikuwa kumi na mitatu. Miji kumi ya eneo la nusu ya kabila la Manase ilitolewa kwa sehemu iliyobaki ya ukoo wa Kohathi kwa kura kulingana na jamaa zao. Ukoo wa Gershomu, kulingana na jamaa zake ulipewa miji kumi na mitatu katika kabila la Isakari, na katika kabila la Naftali na katika kabila la Manase katika Bashani. Vivyo hivyo, miji kumi na miwili katika kabila la Reubeni, na katika kabila la Gadi na katika kabila la Zebuluni ilipewa ukoo wa Merari kulingana na jamaa zao. Kwa njia hii watu wa Israeli waliwapa Walawi miji ili waishi humo pamoja na malisho ya miji hiyo. (Miji iliyotajwa majina hapa juu katika kabila la Yuda, na katika kabila la Simeoni na katika kabila la Benyamini iligawiwa kabila la Lawi kwa kura.) Jamaa nyingine za ukoo wa Kohathi zilipewa miji pamoja na malisho yake katika kabila la Efraimu: Shekemu, mji wa makimbilio katika nchi ya milima ya Efraimu pamoja na malisho yake, Gezeri pamoja na malisho yake, Yokmeamu pamoja na malisho yake, Beth-horoni pamoja na malisho yake; Aiyaloni pamoja na malisho yake, na Gath-rimoni pamoja na malisho yake. Katika nusu ya kabila la Manase walipewa miji ya Aneri pamoja na malisho yake, na Bileamu pamoja na malisho yake. Hii ndiyo miji iliyopewa jamaa za ukoo wa Kohathi. Jamaa za ukoo wa Gershomu walipewa miji ifuatayo pamoja na malisho yake: Katika nusu ya kabila la Manase walipewa: Golani katika Bashani pamoja na malisho yake, Ashtarothi pamoja na malisho yake. Katika kabila la Isakari walipewa: Kedeshi pamoja na malisho yake, Deberathi pamoja na malisho yake, Ramothi pamoja na malisho yake na Anemu pamoja na malisho yake. Katika kabila la Asheri walipewa: Mashali pamoja na malisho yake, Abdoni pamoja na malisho yake, Hukoki pamoja na malisho yake, na Rehobu na malisho yake. Katika kabila la Naftali: Kedeshi katika Galilaya pamoja na malisho yake, Hamoni pamoja na malisho yake na Kiriathaimu pamoja na malisho yake. Jamaa za Merari zilizosalia, zilipewa miji ifuatayo pamoja na malisho yake kandokando ya miji hiyo: Katika kabila la Zebuluni walipewa Rimono pamoja na malisho yake na Tabori pamoja na malisho yake. Katika kabila la Reubeni, mashariki ya mto Yordani karibu na mji wa Yeriko walipewa Bezeri ulioko katika nyanda za juu pamoja na malisho yake, Yahasa pamoja na malisho yake, Kedemothi pamoja na malisho yake na Mefaathi pamoja na malisho yake. Katika kabila la Gadi walipewa Ramothi katika Gileadi pamoja na malisho yake, Mahanaimu pamoja na malisho yake, Heshboni pamoja na malisho yake na Yazeri pamoja na malisho yake. Wana wa Isakari walikuwa wanne: Tala, Pua, Yashubu na Shimroni. Wana wa Tola walikuwa: Uzi, Refaya, Yerieli, Yamai, Ibsamu na Shemueli. Hao walikuwa wakuu wa jamaa za koo za Tola na watu mashujaa sana wa vita nyakati zao. Idadi ya wazawa wao siku za mfalme Daudi ilikuwa 22,600. Uzi alikuwa na mwana mmoja, jina lake Izrahia. Na wana wa Izrahia walikuwa Mikaeli, Obadia, Yoeli na Ishia, jumla wanne, na wote walikuwa wakuu wa jamaa. Kwa vile ambavyo wake na watoto wao walikuwa wengi sana, mliweza kupatikana vikosi vya wanajeshi 36,000 kutokana na wazawa wao. Ndugu zao katika jamaa zote za kabila la Isakari walioandikishwa kwa kufuata koo, walikuwa 87,000, na wote walikuwa mashujaa wa vita. Benyamini alikuwa na wana watatu: Bela, Bekeri na Yediaeli. Bela alikuwa na wana watano: Esboni, Uzi, Uzieli, Yeremothi na Iri. Hawa walikuwa viongozi wa jamaa zao, na wanajeshi mashujaa. Walioandikishwa kwa kufuata koo, idadi ya wazawa wao ilikuwa 22,034. Bekeri alikuwa na wana tisa: Zemira, Yoashi, Eliezeri, Eliehonai, Omri, Yeremothi, Abiya, Anathothi na Alemethi. Wote hawa ni wazawa wa Bekeri. Waliandikishwa kwa koo kulingana na vizazi vyao kama viongozi wa jamaa zao, na idadi ya wazawa wao ilikuwa 20,200, wote wakiwa mashujaa wa vita. Yediaeli alikuwa na mwana mmoja, jina lake Bilhani. Bilhani alikuwa na wana: Yeushi, Benyamini, Ehudi, Kenaana, Zethani, Tarshishi na Ahishahari. Wote hawa walikuwa wakuu wa jamaa katika koo zao na askari mashujaa wa vita. Kutokana na wazawa wao, kulipatikana wanaume 178,200, wanajeshi hodari tayari kabisa kwa vita. Shupimu na Hupimu pia walikuwa wa kabila hili. Dani alikuwa na mwana mmoja, jina lake Hushimu. Naftali alikuwa na wana wanne: Yaasieli, Guni, Yereri na Shalumu. Hao walikuwa wazawa wa Bilha. Manase alikuwa na wana wawili kutokana na suria wake Mwaramu: Asrieli na Makiri. Makiri alikuwa baba yake Gileadi. Makiri aliwazaa Hupimu na Shupimu. Jina la dada yake lilikuwa Maaka. Mwana wa pili wa Makiri alikuwa Selofehadi. Selofehadi alikuwa na mabinti peke yake. Maaka mkewe Makiri, alizaa mwana jina lake Pereshi. Jina la nduguye Pereshi lilikuwa Shereshi. Wanawe Shereshi walikuwa Ulamu na Rakemu. Rakemu alimzaa Bedani. Hawa wote ni wazawa wa Gileadi, mwana wa Makiri, mjukuu wa Manase. Hamo-lekethi, dada yake Gileadi, aliwazaa Ishhodi, Abiezeri na Mala. Wana wa Shemida walikuwa Ahiani, Shekemu, Liki na Aniamu. Hawa ndio wazawa wa Efraimu kutoka kizazi hadi kizazi: Shuthela, Beredi, Tahathi, Eleada, Tahathi, Zabadi na Shuthela. Mbali na Shuthela, Efraimu alikuwa na wana wengine wawili, Ezeri, na Eleadi, ambao waliuawa na wenyeji wa asili wa nchi ya Gathi kwa sababu walikwenda huko kuwanyanganya mifugo yao. Efraimu baba yao aliomboleza vifo vyao kwa siku nyingi sana, na ndugu zake wakaja kumfariji. Ndipo Efraimu akalala na mkewe, naye akachukua mimba na kuzaa mwana. Efraimu akampa jina Beria, kwa sababu ya maafa yaliyoipata jamaa yake. Efraimu alikuwa na binti jina lake Sheera. Huyu ndiye aliyeijenga miji ya Beth-horoni ya juu na chini, na Uzen-sheera. Efraimu alimzaa pia Refa ambaye alimzaa Reshefu, Reshefu akamzaa Tela, Tela akamzaa Tahani, Tahani akamzaa Ladani, Ladani akamzaa Amihudi, Amihudi akamzaa Elishama, Elishama akamzaa Nuni, Nuni akamzaa Yoshua. Milki zao na makao yao yalikuwa: Betheli na vitongoji vyake, Naraani uliokuwa upande wa mashariki, Gezeri uliokuwa upande wa magharibi pamoja na vitongoji vyake, Shekemu na vitongoji vyake, na Aya na vitongoji vyake. Na pia mipakani mwa wana wa Manase: Beth-sheani na vitongoji vyake, Taanaki na vitongoji vyake, Megido na vitongoji vyake na Dori na vitongoji vyake. Hiyo ndiyo miji walimoishi wazawa wa Yosefu, mwana wa Israeli. Hawa ndio wazawa wa Asheri. Asheri alikuwa na wana wanne: Imna, Ishva, Ishri na Beria, na binti mmoja jina lake Sera. Beria alikuwa na wana wawili: Heberi na Malkieli, aliyekuwa baba yake Birzaithi. Heberi alikuwa na wana watatu: Yafleti, Shomeri na Hothamu, na binti mmoja jina lake Shua. Yafleti pia alikuwa na wana watatu: Pasaki, Bimhali na Ashvathi. Shemeri, nduguye, alikuwa na wana watatu: Roga, Yehuba na Aramu. Na Helemu, ndugu yake mwingine, alikuwa na wana wanne: Sofa, Imna, Sheleshi na Amali. Wana wa Sofa walikuwa Sua, Harneferi, Shuali, Beri, Imra, Bezeri, Hodu, Shama, Shilsha, Ithrani na Beera. Wana wa Yetheri walikuwa Yefune, Pispa na Ara. Wana wa Ula walikuwa Ara, Hanieli na Risia. Hao wote walikuwa wazawa wa Asheri na walikuwa wakuu wa jamaa zao, watu wateule na hodari wa vita. Idadi ya wale walioandikishwa kwa kufuata koo katika jeshi ilikuwa 26,000. Benyamini alikuwa na wana watano: Bela, mzaliwa wake wa kwanza, Ashbeli wa pili, Ahara wa tatu, Noha wa nne na Rafa wa tano. Bela naye alikuwa na wana: Adari, Gera, Abihudi, Abishua, Naamani, Ahoa, Gera, Shufamu na Huramu. Hawa ndio wazawa wa Ehudi. Hawa walikuwa viongozi wa jamaa za wale waliokuwa wakiishi Geba, lakini wakachukuliwa mateka uhamishoni Manahathi; Naamani, Ahiya na Gera. Gera, baba yake Uza na Ahihudi, ndiye aliyewaongoza kuchukua hatua hiyo. Shaharaimu aliwapa talaka wake zake wawili, Hushimu na Baara na baadaye alipata watoto wa kiume nchini Moabu. Alimwoa Hodeshi, naye akamzalia wana saba: Yoabu, Sibia, Mesha, Malkamu, Yeuzi, Sakia, na Mirma. Hawa wanawe wote walikuja kuwa wakuu wa koo. Shaharaimu na mkewe Hushimu alipata wana wengine wawili: Abitubu na Elpaali. Wana wa Elpaali walikuwa watatu: Eberi, Mishamu na Shemedi ambaye aliijenga miji ya Ono na Lodi, pamoja na vijiji kandokando yake. Beria na Shema walikuwa miongoni mwa jamaa ambazo zilikuwa zinaishi katika mji wa Aiyaloni, na kuwafukuza wenyeji wa Gathi. Nao Ahio, Shashaki, Yeremothi, Zebadia, Aradi, Ederi, Mikaeli, Ishpa na Yoha ni wazawa wengine wa Beria. Zebadia, Meshulamu, Hizki, Heberi, Ishnerai, Izlia na Yobabu walikuwa wazawa wa Epaali. Yakimu, Zikri, Zabdi, Elienai, Zilethai, Elieli, Adaya, Beraya na Shimrathi walikuwa wazawa wa Shimei. Ishpani, Eberi, Elieli, Abdoni, Zikri, Hanani, Hanania, Elamu, Anthothiya, Ifdeya na Penueli walikuwa wazawa wa Shashaki. Shamsherai, Sheharia, Athalia, Yaareshia, Elia na Zikri walikuwa baadhi ya wazawa wa Yerohamu. Hao ndio waliokuwa wakuu wa koo zao kulingana na vizazi vyao. Walikuwa wakuu na waliishi Yerusalemu. Yeieli, alikuwa mwanzilishi wa mji wa Gibeoni. Mkewe alikuwa Maaka. Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Abdoni. Wanawe wengine ni Zuri, Kishi, Baali, Nadabu, Gedori, Ahio, Zekeri, na Miklothi baba yake Shimea. Hawa pia waliishi Yerusalemu karibu na watu wengine wa ukoo wao. Neri alimzaa Kishi, Kishi akamzaa Shauli. Shauli alikuwa na wana wanne: Yonathani, Malki-shua, Abinadabu na Eshbaali. Yonathani alimzaa Merib-baali, na Merib-baali akamzaa Mika. Mika alikuwa na wana wanne: Pithoni, Meleki, Terea na Ahazi. Ahazi alimzaa Yehoada. Naye Yehoada aliwazaa Alemethi, Azmawethi na Zimri. Zimri alimzaa Mosa. Mosa alimzaa Binea, aliyemzaa Rafa, aliyemzaa Eleasa, naye Eleasa akamzaa Aseli. Wana wa Aseli walikuwa sita: Majina yao ni Azrikamu, Bokeru, Ishmaeli, Shearia, Obadia na Hanani. Wote hawa walikuwa wana wa Aseli. Nao wana wa Esheki, nduguye Aseli, walikuwa watatu. Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Ulamu, wa pili Yeushi na wa tatu Elifeleti. Wana wa Ulamu walikuwa watu mashujaa sana wa vita, na wapiga upinde hodari. Alikuwa na wana na wajukuu wengi, jumla150. Hao wote waliotajwa hapo juu walikuwa wa ukoo wa Benyamini. Hivyo, watu wote wa Israeli waliandikishwa katika nasaba, na orodha hiyo imeandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Israeli. Watu wa Yuda walikuwa wamechukuliwa mateka hadi Babuloni kwa sababu ya kutokuwa waaminifu. Watu wa kwanza kuyarudia makazi yao katika miji yao walikuwa raia wa kawaida, makuhani, Walawi na watumishi wa hekaluni. Baadhi ya watu wa makabila ya Yuda, Benyamini, Efraimu na Manase walikwenda kuishi mjini Yerusalemu: Uthai mwana wa Amihudi, mwana wa Omri, mwana wa Imri, mwana wa Bani, wa wana wa Peresi, mwana wa Yuda. Na wazawa wa Shilo, Asaya mzaliwa wa kwanza, kiongozi na wanawe. Na wazawa wa Zera, Yeueli, na ndugu zao; watu 690. Na wa wazawa wa Benyamini: Salu mwana wa Meshulamu, mwana wa Hodavia, mwana wa Hasenua; na Ibneya mwana wa Yerohamu, Ela, mwana wa Uzi, mwana wa Mikri; na Meshulamu, mwana wa Shefatia, mwana wa Reueli, mwana wa Ibniya; na ndugu zao, sawasawa na vizazi vyao; watu956. Watu hao wote ndio waliokuwa wakuu wa koo za baba zao, kwa kadiri ya koo za baba zao. Makuhani wafuatao waliishi Yerusalemu: Yedaya, Yehoyaribu na Yakini, na Azaria mwana wa Hilkia, mwana wa Meshulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayothi, mwana wa Ahitubu, mkuu wa nyumba ya Mungu; na Adaya, mwana wa Yerohamu, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkiya; na Maasai, mwana wa Adieli, mwana wa Yazera, mwana wa Meshulamu, mwana wa Meshilemithi, mwana wa Imeri; wakuu wa koo za baba zao; pamoja na ndugu zao; jumla watu 1,760. Walikuwa wakuu wenye uwezo mkubwa katika huduma yote ya nyumba ya Mungu. Walawi wafuatao waliishi Yerusalemu: Shemaya, mwana wa Hashubu, mwana wa Azrikamu, mwana wa Hashabia, wa wana wa Merari; na Bakbakari, na Hereshi, na Galali, Matania, mwana wa Mika, mwana wa Zikri, mwana wa Asafu; na Obadia, mwana wa Shemaya, mwana wa Galali, mwana wa Yeduthuni; na Berekia, mwana wa Asa, mwana wa Elkana; waliokuwa wakiishi katika vijiji vya Wanetofathi. Walinzi wa hekalu wafuatao pia waliishi katika Yerusalemu: Shalumu, Akubu, Talmoni na Ahimani na ndugu zao. Shalumu alikuwa mkuu wao. Hadi kufikia wakati huo, walinzi kutoka katika koo zao ndio waliolinda Lango la mfalme la upande wa mashariki. Hapo awali, walikuwa walinzi wa maingilio ya makambi ya Walawi. Shalumu, mwana wa Kore, mwana wa Ebiasafu, pamoja na ndugu zake wa ukoo wa Kora, walikuwa na wajibu wa kuyatunza maingilio ya hema la mkutano, kama vile walivyokuwa babu zake wakati wa ulinzi wa kambi ya Mwenyezi-Mungu. Finehasi, mwana wa Eleazari, alikuwa msimamizi wao, hapo awali, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye. Zekaria mwana wa Meshelemia, pia alikuwa mlinzi wa maingilio ya hema la mkutano. Jumla, watu 212 walichaguliwa kuwa walinzi wa maingilio ya hekalu. Waliandikishwa kulingana na vijiji walimoishi. Mfalme Daudi na Samueli mwonaji ndio waliowathibitisha katika wadhifa huu muhimu. Basi, watu hao na wazawa wao, waliendelea kuyalinda malango ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kila upande, yaani mashariki, magharibi, kaskazini na kusini, palikuwa na lango lililokuwa na walinzi. Walinzi hawa walisaidiwa na ndugu zao waliokuwa wakiishi vijijini, ambao walilazimika kushika zamu ya ulinzi kwa muda wa siku saba, mara kwa mara, kwa maana wale walinzi wakuu wanne, ambao walikuwa Walawi, walikuwa na wajibu wa kusimamia vyumba na hazina ya nyumba ya Mungu. Wao waliishi karibu na nyumba ya Mungu kwa sababu ilikuwa ni wajibu wao kuyalinda na kuyafungua malango yake kila siku asubuhi. Baadhi ya Walawi walisimamia vyombo vilivyotumika wakati wa ibada. Walihitajika kuvihesabu wakati vilipotolewa na wakati viliporudishwa. Wengine walichaguliwa kuvisimamia vifaa vya hekalu, na vyombo vyote vitakatifu, na unga safi, divai, mafuta ya zeituni, ubani na manukato. Lakini kazi ya kutayarisha manukato ilifanywa na makuhani. Metithia, mmoja wa Walawi aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Shalumu, wa ukoo wa Kora, alisimamia utengenezaji wa tambiko ya mikate myembamba. Nao ndugu zao wengine wa ukoo wa Kohathi walikuwa na wajibu wa kutayarisha mikate ya wonyesho kwa ajili ya hekalu kila Sabato. Jamaa nyingine za Walawi zilisimamia huduma ya nyimbo hekaluni. Waliishi katika baadhi ya majengo ya nyumba ya Mungu na hawakuhitajika kufanya kazi nyingine yoyote kwa maana walikuwa kazini usiku na mchana. Watu wote hawa waliotajwa walikuwa viongozi wa kabila la Walawi, kulingana na koo zao. Wao ndio viongozi walioishi Yerusalemu. Yeieli alikuwa mwanzilishi wa mji wa Gibeoni ambamo aliishi yeye pamoja na mkewe, jina lake Maaka. Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Abdoni, naye alifuatiwa na Zuri, Kishi, Baali, Neri, Nadabu, Gedori, Ahio, Zekaria na Miklothi. Miklothi alimzaa Shimeamu. Wazawa wao waliishi Yerusalemu karibu na jamaa nyingine za koo zao. Neri alimzaa Kishi, naye Kishi akamzaa Shauli. Shauli alikuwa na wana wanne: Yonathani, Malki-shua, Abinadabu na Eshbaali. Yonathani alimzaa Merib-baali, Merib-baali akamzaa Mika. Mika alikuwa na wana wanne: Pithoni, Meleki, Tarea na Ahazi. Ahazi alimzaa Yara, Yara akawazaa Alemethi, Azmawethi na Zimri, naye Zimri akamzaa Mosa, Mosa akamzaa Binea, Binea akamzaa Refaya, Refaya akamzaa Eleasa, naye Eleasa akamzaa Aseli. Aseli alikuwa na wana sita: Azrikamu, Bokeru, Ishmaeli, Shearia, Obadia na Hamani. Hawa wote walikuwa wana wa Aseli. Basi, Wafilisti walipigana vita dhidi ya Waisraeli; nao Waisraeli walikimbia mbele ya Wafilisti na kuuawa katika mlima wa Gilboa. Lakini Wafilisti wakamzingira Shauli na wanawe, kisha wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-shua wana wa Shauli. Vita vilikuwa vikali sana dhidi ya Shauli. Wapiga mishale walipomwona walimjeruhi. Ndipo Shauli alipomwambia mtu aliyembebea silaha, “Chomoa upanga wako unichome nife, ili watu hawa wasiotahiriwa wasije wakanidhihaki.” Lakini huyo aliyembebea silaha hakuthubutu; kwa sababu aliogopa sana. Hivyo, Shauli alichukua upanga wake mwenyewe akauangukia. Halafu yule aliyembebea silaha alipoona kuwa Shauli amekufa, naye pia akauangukia upanga wake, akafa. Hivyo ndivyo Shauli alivyokufa, yeye na wanawe watatu, na jamaa yake yote. Nao watu wa Israeli walioishi bondeni walipoona jeshi limewakimbia maadui, na ya kuwa Shauli na wanawe wamekufa, waliihama miji yao wakakimbia. Wafilisti wakaenda na kukaa katika miji hiyo. Kesho yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa, waliikuta maiti ya Shauli na wanawe mlimani Gilboa. Walimvua mavazi, wakachukua kichwa chake pamoja na silaha zake, halafu walituma wajumbe katika nchi yote ya Filistia kutangaza habari njema kwa sanamu zao na watu. Waliziweka silaha za Shauli katika hekalu la miungu yao; kisha wakakitundika kichwa chake katika hekalu la Dagoni. Lakini watu wa Yabesh-gileadi waliposikia yote Wafilisti waliyomtendea Shauli, mashujaa wote waliondoka na kuuchukua mwili wa Shauli na miili ya wanawe, wakaileta mpaka Yabeshi. Wakaizika mifupa yao chini ya mwaloni huko Yabeshi, nao wakafunga kwa muda wa siku saba. Shauli alikufa kwa sababu ya kutokuwa mwaminifu; hakuwa mwaminifu kwani hakutii neno la Mwenyezi-Mungu na alikwenda kwa mwaguzi kumtaka shauri, badala ya kumwendea Mwenyezi-Mungu ili kumtaka shauri. Kwa sababu hiyo Mwenyezi-Mungu akamuua, na ufalme wake akampa Daudi mwana wa Yese. Kisha Waisraeli wote walikusanyika pamoja kwa Daudi huko Hebroni, wakamwambia: “Tazama, sisi ni mwili na damu yako. Hapo awali, Shauli alipokuwa mfalme wewe ndiwe uliyewaongoza Waisraeli vitani, na Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alikuambia, ‘Utakuwa mchungaji wa watu wangu Israeli, na utakuwa mkuu wa watu wangu Israeli.’ Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni; naye Daudi akafanya agano nao mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Waisraeli kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu lililotolewa kwa njia ya Samueli.” Baadaye Daudi na Waisraeli wote walikwenda Yerusalemu uliojulikana kama Yebusi, na ambao wenyeji wake walikuwa Wayebusi. Wakazi wa Yebusi walimwambia Daudi, “Hutaingia katika mji huu.” Hata hivyo, Daudi aliiteka ngome ya Siyoni, yaani mji wa Daudi. Ndipo Daudi akasema, “Mtu atakayetangulia kuwapiga Wayebusi, atakuwa mkuu na kamanda jeshini.” Basi Yoabu, mwana wa Seruya, akawa wa kwanza kuwashambulia, hivyo akawa mkuu. Daudi alikaa katika ngome hiyo, na kwa hiyo, mji huo ukaitwa “Mji wa Daudi.” Aliujenga mji huo, akianzia Milo, na kuuzunguka wote, na Yoabu akautengeneza mji huo upya. Naye Daudi akazidi kuwa mkuu kwa sababu Mwenyezi-Mungu wa majeshi alikuwa pamoja naye. Hii ndiyo orodha ya wakuu wa mashujaa wa Daudi, ambao pamoja na watu wengine wote wa Israeli, walimuunga mkono kwa pamoja ili awe mfalme, sawa na neno la Mwenyezi-Mungu alilotoa juu ya Waisraeli. Ifuatayo ni orodha ya mashujaa hao wa Daudi: Yashobeamu, Mhakmoni, aliyekuwa kiongozi wa “Wale thelathini.” Yeye alipigana kwa mkuki wake akaua watu 300 kwa mara moja vitani. Halafu aliyefuata miongoni mwa wale mashujaa watatu alikuwa Eleazari mwana wa Dodo, Mwahohi. Siku moja Eleazari alikuwa pamoja na Daudi huko Pas-damimu, wakati Wafilisti walipokusanyika kupigana vita. Huko kulikuwa na shamba lenye shayiri tele, nao Waisraeli walikuwa wamewakimbia Wafilisti. Lakini Daudi na Eliazari walisimama imara katikati ya shamba hilo ili kulitetea, wakawaua Wafilisti; Mwenyezi-Mungu akawaokoa kwa kuwapa ushindi mkubwa. Kisha mashujaa watatu kati ya wakuu thelathini waliteremka hadi kwenye mwamba, wakamwendea Daudi kwenye pango huko Adulamu. Wakati huo jeshi la Wafilisti lilikuwa limepiga kambi katika bonde la Refaimu. Naye Daudi wakati huo alikuwa katika ngome, nalo jeshi la Wafilisti lilikuwa mjini Bethlehemu. Daudi akasema kwa hamu kubwa, “Laiti kama mtu angeweza kunipa maji ya kunywa kutoka katika kisima cha Bethlehemu kilicho karibu na lango la mji!” Wale mashujaa wake watatu walitoka, wakapenya katikati ya kambi ya jeshi la Wafilisti, wakaenda na kuchota maji katika kisima cha Bethlehemu, karibu na lango la mji, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa, na badala yake akayamwaga chini kama tambiko kwa Mwenyezi-Mungu akisema, “Tendo kama hili lipitishie mbali nami; siwezi kulifanya mbele ya Mungu wangu. Je, waweza kunywa damu ya maisha ya watu hawa? Maana kwa kuyahatarisha maisha yao walileta maji haya.” Kwa hiyo Daudi hakuyanywa maji hayo. Hayo ndio mambo waliyotenda wale mashujaa watatu. Abishai, nduguye Yoabu, alikuwa mkuu wa mashujaa thelathini. Yeye alipigana kwa mkuki wake dhidi ya watu 300, akawaua, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. Basi, akawa mashuhuri zaidi miongoni mwa mashujaa thelathini, hata akawa kamanda wao, lakini hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu. Naye Benaya, mwana wa Yehoyada, kutoka Kabzeeli, alikuwa askari shujaa ambaye alifanya mambo mengi ya ajabu. Aliwaua mashujaa wawili kutoka Moabu, na siku moja wakati wa barafu, alishuka na kuua simba shimoni. Vilevile, alimuua Mmisri mmoja, mtu mrefu sana, urefu wake kama mita mbili, naye mkononi mwake alikuwa amebeba mkuki mkubwa sana, kama mti wa mfumaji. Lakini Benaya alimwendea akiwa na fimbo tu, akamnyanganya mkuki huo, na kumuua Mmisri huyo kwa mkuki wake mwenyewe. Benaya, mwana wa Yehoyada alifanya mambo haya, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. Basi, akawa mashuhuri kati ya wale mashujaa thelathini, ingawa hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu. Na Daudi akampa cheo cha mkuu wa walinzi wake binafsi. Wanajeshi mashujaa wa Daudi walikuwa: Asaheli nduguye Yoabu, Elhanani mwana wa Dodo wa Bethlehemu, Shamothi Mharodi, Helesi Mpeloni, Ira, mwana wa Ikeshi Mtekoa, Abiezeri Mwanathothi; Sibekai Mhushathi; Ilai Mwahohi; Maharai Mnetofathi; Heledi, mwana wa Baana Mnetofathi; Itai, mwana wa Ribai, kutoka Gibea, wa kabila la Benyamini; Benaya Mpirathoni; Hurai kutoka vijito vya Gaashi, Abieli Mwaibathi; Azmawethi Mbaharumu; Eliaba Mshaalboni; wana wa Yasheni Mgiloni; Yonathani, mwana wa Shagee Mharari, Ahiamu, mwana wa Sakari Mharari; Elifali, mwana wa Uri; Heferi Mmekerathi; Ahiya Mpeloni; Hezro Mkarmeli; Naarai, mwana wa Ezbai; Yoeli, nduguye Nathani; Mibhari, mwana wa Hagri; Zeleki Mwamoni; Naharai Mbeerothi, aliyekuwa mbeba silaha wa Yoabu, mwana wa Seruya; Ira na Garebu, waliokuwa Waithri, Uria, Mhiti; Zabadi, mwana wa Ahlai; Adina, mwana wa Shiza Mreubeni, mkuu wa Wareubeni, akiwa pamoja na watu thelathini; Hanani, mwana wa Maaka, Yoshafati Mmithni; Uzia Mwashterathi, Shama na Yeieli, wana wa Hothamu Mwaroeri; Yediaeli na Yoha nduguye, wana wa Shimri Mtizi; Elieli Mmahawi, Yeribai na Yoshavia wana wa Elnaamu; Ithma Mmoabu; Elieli, Obedi, na Yaasieli Mmesobai. Hawa ni wanaume ambao walijiunga na Daudi huko Siklagi, alipokuwa hana uhuru wowote wa kutembea kwa sababu ya mfalme Shauli mwana wa Kishi; walikuwa miongoni mwa askari mashujaa waliomsaidia vitani. Hao walikuwa watu wa kabila la Benyamini kama alivyokuwa Shauli. Walikuwa wapiga upinde hodari, na warusha mawe kwa kombeo kwa kutumia mikono yote, wa kulia na kushoto. Kiongozi wao alikuwa Ahiezeri, aliyesaidiwa na Yoashi, wote wana wa Shemaa kutoka Gibea; wengineo ni: Yezieli na Peleti, wana wa Azmawethi, Beraka, Yehu kutoka Anathothi, Ishmaya kutoka Gibeoni, mtu shujaa miongoni mwa wale thelathini na kiongozi wao pia pamoja na Yeremia, Yahazieli, Yohanani, Yozabadi kutoka Gedera, Eluzai, Yeremothi, Bealia, Shemaria, Shefatia, Mharufi, Elkana, Ishia, Azareli, Yoezeri, Yashobeamu kutoka ukoo wa Kora na Yoela na Zebadia, wana wa Yerohamu, kutoka Gedori. Tena, watu kutoka kabila la Gadi walijiunga na Daudi akiwa ngomeni kule nyikani. Hawa walikuwa askari wenye nguvu na uzoefu, hodari wa kutumia ngao na mkuki; wenye nyuso za kutisha kama simba na wepesi kama swala milimani. Kiongozi wao mkuu alikuwa Ezeri, wa pili Obadia, wa tatu Eliabu, wa nne Mishmana, wa tano Yeremia, wa sita Atai, wa saba Elieli, wa nane Yohanani, wa tisa Elsabadi, wa kumi Yeremia, na wa kumi na moja Makbanai. Wagadi hao, walikuwa maofisa wa jeshi. Kulingana na vyeo vyao, mdogo alisimamia kikosi cha wanajeshi 100, na mkubwa alisimamia kikosi cha wanajeshi 1,000. Hawa ndio watu waliovuka mto Yordani mnamo mwezi wa kwanza, mto ulipokuwa umefurika pande zote na kuwatawanya watu mashariki na magharibi ya mto. Baadhi ya watu kutoka makabila ya Benyamini na Yuda walifika ngomeni alipokuwa Daudi. Daudi akatoka nje kuwalaki, akawaambia, “Ikiwa mmekuja kwangu kama marafiki ili kunisaidia basi nawapokea kwa moyo wote, lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa maadui zangu, ingawa sijatenda ovu lolote, Mungu wa baba zetu awaone na awakemee.” Hapo Roho akamjia Abishai, mkuu wa hao watu thelathini, naye akasema, “Sisi tu watu wako, ee Daudi, tuko upande wako, ee mwana wa Yese! Amani, amani iwe kwako, na amani iwe kwa yeyote akusaidiaye! Maana akusaidiaye ndiye Mungu wako.” Ndipo Daudi akawapokea na kuwafanya maofisa katika jeshi lake. Askari wengine wa kabila la Manase, walitoroka na kujiunga na Daudi, wakati alipoondoka pamoja na Wafilisti kwenda kupigana na mfalme Shauli. (Lakini hata hivyo, hakuwasaidia maana watawala wa Wafilisti walifanya shauri wamfukuze arudi Siklagi wakisema, “Tutayahatarisha maisha yetu kwa sababu atatutoroka arudi kwa bwana wake Shauli.”) Basi, Daudi alipokuwa Siklagi, watu wafuatao wa kabila la Manase walimwendea: Adna, Yozabadi, Yediaeli, Mikaeli, Yozabadi, Elihu na Silethai. Kila mmoja wao alikuwa kiongozi wa kikosi cha watu 1,000 katika kabila la Manase. Walimsaidia Daudi kupigana na magenge ya washambuliaji, kwani wote walikuwa askari mashujaa na makamanda jeshini. Siku hata siku, watu walijiunga na Daudi kumsaidia, hatimaye akawa na jeshi kubwa sana, kama jeshi la Mungu. Hii ndio idadi ya vikosi vya askari wenye silaha waliojiunga na Daudi huko Hebroni ili kumtwalia ufalme kutoka kwa Shauli, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu: Watu wa kabila la Yuda waliokuwa na mikuki na ngao, walikuwa 6,800. Wote walikuwa na silaha zao. Kutoka kabila la Simeoni, watu 7,100 mashujaa na wenye ujuzi mwingi wa vita. Kutoka kabila la Lawi: Watu 4,600. Yehoyada, wa uzao wa Aroni na wenzake: Watu 3,700. Jamaa ya Sadoki, kijana hodari vitani, yeye pamoja na makamanda ishirini na wawili kutoka ukoo wa baba yake mwenyewe. Kutoka kabila la Benyamini, (kabila la Shauli): Watu 3,000. Wengi wao walibaki waaminifu kwa jamaa ya Shauli; Kutoka kabila la Efraimu: Watu 20,800, watu mashujaa sana tena mashuhuri katika koo zao; Kutoka nusu ya kabila la Manase: Watu 18,000, waliotajwa majina ili waje kumtawaza Daudi awe mfalme. Kutoka kabila la Isakari: Wakuu 200 pamoja na ndugu zao wote waliokuwa chini ya amri yao. Wakuu hao walikuwa na elimu ya kujua mambo ya nyakati na walijua kilichowapasa Waisraeli kufanya. Kutoka kabila la Zebuluni: Watu 50,000; waaminifu na wazoefu wa vita. Walijiandaa na zana za vita za kila namna, lengo lao likiwa ni kumsaidia Daudi tu. Kutoka kabila la Naftali: Makamanda 1,000 pamoja na watu 37,000 wenye ngao na mikuki. Kutoka kabila la Dani: Watu 28,600 wenye silaha tayari kwa vita. Kutoka kabila la Asheri: Watu 40,000 wazoefu wa vita, tayari kwa mapigano. Kutoka kabila la Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kutoka ngambo ya mto Yordani: Watu 120,000 wenye kila aina ya silaha za vita. Wanajeshi hao wote, waliojiandaa tayari kabisa kwa vita, walikwenda Hebroni na nia yao kubwa ikiwa ni kumtawaza Daudi awe mfalme wa Israeli yote. Nao watu wote wa Israeli, pia waliungana wakiwa na nia moja ya kumtawaza Daudi awe mfalme. Basi, walikaa na Daudi kwa muda wa siku tatu, wakila na kunywa kwani ndugu zao walikuwa wamekwisha waandalia vyakula. Zaidi ya hayo, majirani zao wa karibu na hata wa mbali kama huko Isakari, Zebuluni na Naftali, waliwaletea vyakula walivyobeba kwa punda, ngamia, nyumbu na ng'ombe. Waliwaletea unga, mikate ya tini, vichala vya zabibu kavu, divai na mafuta, ng'ombe na kondoo wengi, kukawa na vyakula tele, kwani kulikuwa na furaha katika Israeli. Daudi alishauriana na makamanda wa vikosi vya maelfu na vikosi vya mamia, pamoja na viongozi wote. Kisha akawaambia Waisraeli wote waliokusanyika, “Ikiwa mtakubaliana nami, na ikiwa ni mapenzi yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, na tufanye hivi: Tutume wajumbe waende wakawaite ndugu zetu waliobaki nchini Israeli, pamoja na makuhani na Walawi walioko katika miji yao na malisho yao, waje wajumuike pamoja nasi. Kisha twende tukalichukue sanduku la agano la Mungu wetu, maana hatukulijali wakati wa utawala wa mfalme Shauli.” Watu wote walikubaliana na pendekezo hilo kwani waliliona kuwa jambo jema. Hivyo, Daudi aliwakusanya Waisraeli wote nchini; toka kijito cha Shihori kilichoko Misri, hadi maingilio ya Hamathi ili kulileta sanduku la Mungu toka Kiriath-yearimu. Daudi, akiandamana na Waisraeli wote, akaenda hadi mjini Baala, yaani Kiriath-yearimu, nchini Yudea, ili kulichukua toka huko sanduku la Mungu linaloitwa kwa jina lake Mwenyezi-Mungu akaaye kwenye kiti chake cha enzi juu ya viumbe vyenye mabawa. Basi, wakalichukua sanduku la Mungu kutoka katika nyumba ya Abinadabu kwa gari jipya. Uza na Ahio waliliendesha gari hilo. Daudi na Waisraeli wote wakawa wanacheza kwa nguvu zao zote, mbele ya Mungu. Waliimba huku wanapiga ala za muziki zilizotengenezwa kwa mvinje: Vinubi, vinanda, matari, matoazi na tarumbeta. Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza aliunyosha mkono wake kulishikilia sanduku la agano kwa sababu ng'ombe walijikwaa. Mara Mwenyezi-Mungu akamkasirikia Uza kwa kulishika sanduku, akamuua. Uza akafa papo hapo mbele ya Mungu. Daudi alikasirika kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimuua Uza akiwa na hasira. Kwa sababu hiyo, mahali hapo huitwa Peres-uza hadi leo. Siku hiyo Daudi akamwogopa Mungu, akasema, “Sasa, nitawezaje kulichukua sanduku la Mungu nyumbani mwangu?” Basi, Daudi hakulichukua sanduku mpaka mji wa Daudi, bali alilipeleka nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku hilo la Mungu lilikaa huko kwa Obed-edomu kwa muda wa miezi mitatu, naye Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya Obed-edomu na mali yake yote. Kisha mfalme Hiramu wa Tiro alituma wajumbe kwa Daudi, pia alimpelekea mierezi, waashi na maseremala, ili wamjengee Daudi ikulu. Hivyo, Daudi akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu amemwimarisha awe mfalme wa Israeli, na kwamba ufalme wake umekuzwa kwa ajili ya Israeli, watu wake. Huko Yerusalemu, Daudi alioa wake wengi zaidi, naye akazaa wana na mabinti wengine. Yafuatayo ndio majina ya watoto aliozaa huko Yerusalemu: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, Ibhari, Elishua, Elpeleti, Noga, Nefegi, Yafia, Elishama, Beeliada na Elifeleti. Wafilisti waliposikia kwamba Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa nchi nzima ya Israeli, wote walitoka kwa wingi kwenda kumtafuta. Daudi alipopata habari, alitoka kwenda kuwakabili. Wafilisti walifika wakaanza mashambulizi katika bonde la Refaimu. Ndipo Daudi alipomwuliza Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda, nitawatia mikononi mwako.” Basi, Daudi akaenda huko Baal-perasimu, akawashinda; halafu akasema, “Mungu amepita katikati ya adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji yaendayo kasi.” Kwa hiyo mahali hapo panaitwa Baal-perasimu. Wafilisti walipokimbia, waliziacha sanamu za miungu yao huko, naye Daudi akatoa amri zote zichomwe moto. Kisha Wafilisti walifanya mashambulizi katika bonde hilo kwa mara ya pili. Safari hii, Daudi alipoomba shauri kwa Mungu, Mungu akamwambia, “Usiwashambulie kutoka hapa, ila zunguka na kuwashambulia kutoka mkabala na miti ya miforosadi, halafu washambulie kutoka huko. Na mara utakaposikia vishindo vya gwaride kwenye vilele vya hiyo miforosadi, haya, toka uende vitani. Nitakuwa nimekwisha kukutangulia kulipiga jeshi la Wafilisti.” Daudi alifanya kama alivyoamriwa na Mungu. Alilipiga jeshi la Wafilisti kutoka Gibeoni hadi Gezeri. Daudi akawa maarufu kote nchini, naye Mwenyezi-Mungu akayatia hofu mataifa yote, nayo yakamwogopa sana. Daudi alijijengea nyumba katika mji wa Daudi. Tena akalitengenezea sanduku la Mungu mahali, akalipigia hema. Kisha akasema, “Hakuna mtu mwingine yeyote atakayelibeba sanduku la Mungu isipokuwa Walawi, maana Mwenyezi-Mungu aliwachagua wao kulibeba na kumtumikia milele.” Basi, akawakusanya Waisraeli wote waje Yerusalemu, ili kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu mahali alipolitayarishia. Halafu Daudi akawaita wazawa wa Aroni na Walawi: Kutoka katika ukoo wa Kohathi, wakaja Urieli, pamoja na ndugu zake120 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo wa Merari wakaja Asaya pamoja na ndugu zake 220 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo wa Gershomu, wakaja Yoeli pamoja na ndugu zake 130 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo ya Elisafani, wakaja Shemaya pamoja na ndugu zake 200 chini ya usimamizi wake; kutoka katika ukoo wa Hebroni, wakaja Elieli pamoja na ndugu zake 80 chini ya usimamizi wake; na kutoka katika ukoo wa Uzieli, wakaja Aminadabu pamoja na ndugu zake 112 chini ya usimamizi wake. Daudi akawaita makuhani wawili: Sadoki na Abiathari, na Walawi sita: Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu; akawaambia, “Nyinyi ni viongozi wa koo za Walawi. Jitakaseni pamoja na ndugu zenu, ili mkalilete sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hadi mahali ambapo nimelitayarishia. Kwa sababu hamkulibeba safari ya kwanza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alituadhibu kwani hatukulitunza kama alivyoagiza.” Basi, makuhani na Walawi wakajitakasa ili wapate kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Walawi wakalibeba mabegani mwao wakitumia mipiko yake kama Mose alivyoamuru, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu. Daudi pia aliwaamuru wakuu wa Walawi wachague baadhi ya ndugu zao wawe wakiimba na kupiga ala za muziki: Vinanda, vinubi na matoazi kwa nguvu, ili kutoa sauti za furaha. Hivyo wakachagua watu wafuatao katika koo za waimbaji: Hemani mwana wa Yoeli, Asafu nduguye aliyekuwa mwana wa Berekia na wana wa Merari, ndugu zao, na Ethani mwana wa Kushaya. Kisha wakawachagua Walawi wafuatao wawe wasaidizi wao kwa kushika nafasi ya pili: Zekaria, Yaasieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Benaya, Maaseya, Matithia, Elifelehu na Mikneya na walinzi wa lango: Obed-edomu na Yeieli. Hemani, Asafu na Etani wakachaguliwa kupiga matoazi ya Shaba. Zekaria, Azieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Maaseya na Benaya, walikuwa wapiga vinubi vya sauti ya Alamothi. Lakini Matithia, Elifelehu, Mikneya, Obed-edomu, Yeieli na Azazia waliongoza wakiwa na vinubi vya sauti ya Sheminithi. Naye Kenania kwa sababu ya ujuzi wa muziki aliokuwa nao, aliwekwa kuwa kiongozi wa wote. Berekia na Elkana walikuwa walinzi wa sanduku la agano. Shebania, Yoshafati, Nethaneli, Amasai, Zekaria, Benaya na Eliezeri, waliokuwa makuhani, waliwekwa kupiga tarumbeta mbele ya sanduku la Mungu. Obed-edomu na Yehiya waliwekwa pia kuwa walinzi wa sanduku. Basi, Daudi, wazee wa Waisraeli na makamanda wa maelfu, wakaenda kulichukua sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu kutoka nyumbani kwa Obed-edomu kwa shangwe. Wakamtolea tambiko Mungu: Mafahali saba na kondoo madume saba kwa sababu aliwasaidia wale Walawi waliolibeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Daudi alikuwa amevaa joho la kitani safi, hali kadhalika na Walawi wote waliobeba sanduku, waimbaji na Kenania kiongozi wa waimbaji. Mbali na joho hilo, Daudi alikuwa amevaa kizibao cha kitani. Hivyo, Waisraeli wote walijumuika pamoja kwa shangwe kulichukua sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu hadi Yerusalemu. Walilisindikiza kwa mlio wa baragumu, tarumbeta, matoazi, na sauti kubwa za vinanda na vinubi. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipokuwa linaingia katika mji wa Daudi, Mikali, binti Shauli, alichungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi akicheza na kushangilia, basi akamdharau moyoni mwake. Kisha waliliingiza sanduku la Mungu, na kuliweka ndani ya hema ambayo Daudi alikuwa ameitayarisha. Halafu wakatoa tambiko za kuteketezwa na za amani mbele ya Mungu. Daudi alipomaliza kutoa tambiko hizo za kuteketezwa na za amani, aliwabariki watu katika jina la Mwenyezi-Mungu, na akawagawia Waisraeli wote, wanaume kwa wanawake, kila mmoja akapewa mkate, kipande cha nyama na mkate wa zabibu. Zaidi ya hayo, Daudi aliwateua baadhi ya Walawi wawe wahudumu wa sanduku la Mwenyezi-Mungu, wamtukuze, wamtolee shukrani na wamsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Alimchagua Asafu kuwa kiongozi wao, akisaidiwa na Zekaria. Yeieli, Shemiramothi, Yehieli, Metithia, Eliabu, Benaya, Obed-edomu na Yehieli, aliwachagua wawe wapiga vinanda na vinubi. Asafu alipiga matoazi, nao makuhani Benania na Yaharieli, walichaguliwa wawe wakipiga tarumbeta mfululizo mbele ya sanduku la agano la Mungu. Basi, hiyo ikawa siku ambayo kwa mara ya kwanza, Daudi alimpa Asafu na ndugu zake Walawi wajibu wa kumwimbia Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani. Mpeni shukrani Mwenyezi-Mungu, tangazeni ukuu wake, yajulisheni mataifa mambo aliyoyatenda! Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa; simulieni matendo yake ya ajabu! Jisifieni jina lake takatifu; wenye kumcha Mwenyezi-Mungu na wafurahi. Mwendeeni Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu; mwendeeni Mwenyezi-Mungu daima. Kumbukeni matendo ya ajabu aliyotenda, maajabu yake na hukumu alizotoa, enyi wazawa wa Abrahamu, mtumishi wake, enyi wazawa wa Yakobo, wateule wake. Yeye Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu; hukumu zake zina nguvu duniani kote. Yeye hulishika agano lake milele, hutimiza ahadi zake kwa vizazi elfu. Hushika agano alilofanya na Abrahamu, na ahadi aliyomwapia Isaka. Alimthibitishia Yakobo ahadi yake, akamhakikishia agano hilo la milele. Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani, nayo itakuwa mali yenu wenyewe.” Idadi yenu ilikuwa ndogo, mlikuwa wachache na wageni katika nchi ya Kanaani, mkitangatanga toka taifa hadi taifa, kutoka nchi moja hadi nchi nyingine, Mungu hakumruhusu mtu yeyote awadhulumu; kwa ajili yao aliwaonya wafalme: “Msiwaguse wateule wangu; msiwadhuru manabii wangu!” Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote. Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu. Yatangazieni mataifa utukufu wake, waambieni watu wote matendo yake ya ajabu. Maana Mwenyezi-Mungu ni mkuu, anasifika sana anastahili kuheshimiwa kuliko miungu yote. Miungu yote ya mataifa mengine si kitu; lakini Mwenyezi-Mungu aliziumba mbingu. Utukufu na fahari vyamzunguka, nguvu na furaha vyajaza hekalu lake. Mpeni Mwenyezi-Mungu, heshima enyi jamii zote za watu, naam, kirini utukufu na nguvu yake. Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima ya utukufu wa jina lake; leteni tambiko na kuingia nyumbani mwake. Mwabuduni Mwenyezi-Mungu patakatifuni pake. Ee dunia yote; tetemeka mbele yake! Ameuweka ulimwengu imara, hautatikisika. Furahini enyi mbingu na dunia! Yaambieni mataifa, “Mwenyezi-Mungu anatawala!” Bahari na ivume, pamoja na vyote vilivyomo! Furahini enyi mashamba na vyote vilivyomo! Ndipo miti yote msituni itaimba kwa furaha mbele ya Mwenyezi-Mungu anayekuja naam, anayekuja kuihukumu dunia. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele! Mwambieni Mwenyezi-Mungu: Utuokoe, ee Mungu wa wokovu wetu, utukusanye pamoja na kutuokoa kutoka kwa mataifa, tupate kulisifu jina lako takatifu, kuona fahari juu ya sifa zako. Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele! Kisha watu wote wakasema, “Amina!” Pia wakamsifu Mwenyezi-Mungu. Hivyo, mfalme Daudi akawaacha Asafu na nduguze Walawi mahali walipoliweka sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya huduma zinazotakiwa mbele ya sanduku kila siku. Obed-edomu, mwana wa Yeduthuni, pamoja na wenzake sitini na wanane waliwasaidia. Obed-edomu mwana wa Yeduthuni na Hosa walikuwa walinzi wa malango. Mfalme Daudi akawaweka kuhani Sadoki na makuhani wenzake kuwa wahudumu wa hema ya Mwenyezi-Mungu iliyokuwa mahali pa kuabudu huko Gibeoni ili kutolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka za kuteketezwa daima asubuhi na jioni, kulingana na yote yaliyoandikwa katika sheria ya Mwenyezi-Mungu aliyowaamuru Waisraeli. Pamoja nao walikuwa Hemani na Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa, waliotajwa majina yao, ili kumshukuru Mwenyezi-Mungu kwa kuwa fadhili zake ni za milele. Hemani na Yeduthuni walikuwa na tarumbeta na matoazi kwa ajili ya muziki na ala za muziki kwa ajili ya nyimbo takatifu. Wana wa Yeduthuni walichaguliwa kuyalinda malango. Kisha, kila mtu aliondoka kwenda nyumbani kwake; naye Daudi akaenda nyumbani kwake kuibariki jamaa yake. Wakati mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika ikulu, siku moja alimwita nabii Nathani, na kumwambia, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mwerezi, lakini sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu linakaa hemani.” Nathani akamwambia Daudi, “Fanya chochote unachofikiria moyoni mwako, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.” Lakini usiku uleule, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Nathani, kusema, “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa. Tangu wakati ule nilipowaongoza watu wa Israeli kutoka Misri mpaka hivi leo, sijaishi kwenye nyumba. Nimekuwa nikihama toka hema hadi hema, na toka makao hadi makao mengine. Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli, nimepata kumwuliza mwamuzi wao yeyote niliyemwamuru awachunge watu wangu, “Kwa nini hukunijengea nyumba ya mierezi?” ’ Kwa hiyo basi, mwambie mtumishi wangu Daudi: ‘Mwenyezi-Mungu wa majeshi anasema hivi: Nilikutoa malishoni ulipokuwa unawachunga kondoo, ili uwe mkuu wa watu wangu Israeli. Tangu wakati huo nimekuwa pamoja nawe kokote ulikokwenda na nimewaangamiza maadui zako wote mbele yako. Nitakufanya kuwa maarufu kama wakuu wengine wa dunia. Nami nitawachagulia watu wangu wa Israeli mahali pa kuishi niwapandikize, ili waishi mahali pao wenyewe, wasisumbuliwe tena. Nao watu wakatili wanaotumia nguvu hawatawatesa tena kama hapo awali, tangu wakati nilipowateua waamuzi juu ya watu wangu Israeli; mimi nitawashinda maadui zako wote. Zaidi ya yote, mimi Mwenyezi-Mungu nakutangazia kuwa nitakujengea nyumba. Siku zako zitakapotimia za kujiunga na babu zako, nitamfanya mmoja wa watoto wako, wewe mwenyewe awe mfalme; nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba; nami nitahakikisha kwamba ufalme wake unadumu milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; lakini sitamwondolea fadhili zangu kama vile nilivyomwondolea Shauli aliyekutangulia. Bali nitamwimarisha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele, na kiti chake cha enzi kitakuwa imara daima.’” Nathani alimwelezea Daudi mambo yote haya kulingana na maono yote. Kisha mfalme Daudi akaingia ndani ya hema na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu akaomba, “Mimi ni nani, ee Mwenyezi-Mungu, na nyumba yangu ni nini hata unitukuze hivi? Isitoshe, umenifanyia mengine zaidi: Umenitolea ahadi juu ya vizazi vyangu vijavyo ee Mwenyezi-Mungu! Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi mtumishi wako, kwa kunitukuza hivyo? Wewe unanijua mimi mtumishi wako. Ee Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya mtumishi wako na kwa kufuatana na moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote. Hakuna mwingine kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu, na yote tunayoyasikia yanathibitisha kwamba hakuna Mungu mwingine ila wewe. Tena ni watu gani duniani ambao wanaweza kulinganishwa na watu wako wa Israeli ambao peke yao Mungu wao alikwenda kuwakomboa ili wawe watu wake? Wewe ulijifanyia jina kwa kutenda mambo makubwa na ya ajabu hapo ulipoyafukuza mataifa mbele ya watu wako ambao uliwakomboa kutoka Misri. Hata umejifanyia watu wako wa Israeli kuwa watu wako milele; nawe ee Mwenyezi-Mungu, umekuwa Mungu wao. “Basi sasa, ewe Mwenyezi-Mungu, liimarishe milele neno lako ulilosema kunihusu mimi mtumishi wako na kuhusu jamaa yangu. Nalo jina lako litatukuzwa milele, nao watu watasema, ‘Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, ndiye Mungu wa Israeli!’ Na jamaa yangu, mimi Daudi mtumishi wako, itaimarika mbele yako. Maana ee Mungu wangu nimepata ujasiri kukuomba kwa sababu wewe, umenifunulia ukisema ya kwamba utanijengea nyumba. Sasa ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe Mungu, umeniahidi mimi mtumishi wako jambo hili jema; kwa hiyo nakuomba uibariki nyumba yangu, mimi mtumishi wako, ili idumu milele mbele yako; kwani unachobariki wewe, huwa kimebarikiwa milele.” Baada ya hayo, mfalme Daudi aliwashinda na kuwatiisha Wafilisti. Akauteka mji wa Gathi pamoja na vijiji vyake walivyomiliki Wafilisti. Aliwashinda Wamoabu pia, wakawa watumishi wake na wakawa wanalipa kodi. Daudi pia alimshinda Hadadezeri mfalme wa Soba, nchi iliyokuwa karibu na Hamathi, alifanya hivyo wakati alipokuwa akienda kujisimamishia nguzo ya kumbukumbu kwenye sehemu za mto Eufrate. Daudi akateka magari ya farasi 1,000, askari wapandafarasi 7,000 na wa miguu 20,000. Kisha Daudi alikata mishipa ya miguu ya nyuma ya farasi wote wa magari, ila aliwabakiza 100. Nao Waaramu wa Damasko, walipokwenda kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi aliwashambulia na kuwaua watu 22,000. Halafu Daudi aliweka kambi za kijeshi katika mji wa Shamu ya Damasko. Basi Waaramu wakawa watumishi wake, na wakawa wanalipa kodi. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda. Daudi alizichukua ngao za dhahabu walizobeba wanajeshi wa Hadadezeri, na kuzipeleka Yerusalemu. Daudi alichukua pia shaba nyingi sana kutoka mji wa Tibhathi na mji wa Kuni; iliyokuwa miji ya Hadadezeri. Solomoni aliitumia shaba hiyo kutengenezea nguzo na vyombo vya shaba. Wakati Tou, mfalme wa Hamathi aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri mfalme wa Soba, alituma mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi, kumpelekea salamu na pongezi kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri na kumshinda. Maana Hadadezeri alipigana na Tou mara nyingi. Hadoramu alimpelekea Daudi zawadi za vyombo vya fedha, dhahabu na shaba. Zawadi hizo, mfalme Daudi aliziweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu pamoja na fedha na dhahabu aliyoiteka kutoka mataifa yote kutoka: Edomu, Moabu, Amoni, Filisti na Amaleki. Abishai mwana wa Seruya, aliwaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi. Basi akaweka kambi za kijeshi huko Edomu. Nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Daudi. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda. Hivyo Daudi akatawala juu ya Israeli yote, na akahakikisha ya kwamba watu wake wote wanatendewa haki na usawa. Yoabu, mwana wa Seruya alikuwa mkuu wa majeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mtunza kumbukumbu; Sadoki, mwana wa Ahitubu na Ahimeleki, mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Shausha alikuwa katibu; na Benaya, mwana wa Yehoyada alisimamia askari walinzi Wakerethi na Wapelethi; wana wa Daudi walikuwa maofisa wakuu katika utawala wake. Ikawa baada ya hayo Nahashi, mfalme wa Waamoni akafariki; naye mwanawe akashika utawala. Basi, Daudi akasema, “Nitamtendea mema Hanuni mwana wa Nahashi, kwani baba yake alinitendea mema pia.” Hivyo Daudi alituma wajumbe na kumpelekea salamu za rambirambi kwa ajili ya kifo cha baba yake. Nao wakaenda kwa Hanuni ili kumfariji, huko katika nchi ya Waamoni. Lakini viongozi wa Waamoni wakamwambia mfalme, “Je! Unadhani ni kwa sababu ya heshima ya baba yako ati Daudi ametuma wajumbe hawa waje kukufariji? Watu hawa si majasusi waliotumwa kuja kuichunguza nchi kuiangamiza na kuipeleleza?” Basi Hanuni aliwachukua wajumbe hao wa Daudi, akawanyoa ndevu na kuzipasua nguo zao katikati hadi matakoni, kisha akawatoa waende zao, nao wakaondoka kurudi makwao. Daudi alipopashwa habari jinsi walivyotendewa wajumbe wake, alituma watu kuwalaki kwani hao wajumbe waliona aibu sana. Naye mfalme aliwaambia, “Kaeni mjini Yeriko, hata mtakapoota ndevu, Kisha mrudi.” Waamoni walipoona wamejifanya wachukizwe na Daudi, Hanuni na hao Waamoni walituma watu wapeleke talanta 4,000 za fedha kukodisha magari na wapandafarasi kutoka Mesopotamia, Aramaaka na Soba. Walikodisha magari 32,000 na mfalme wa Maaka na askari wake, akaja na kupiga kambi karibu na Medeba. Waamoni walikusanyika toka kwenye miji yao yote, wakajiandaa tayari kwa vita. Naye Daudi aliposikia habari hizo alimtuma Yoabu na jeshi lote la mashujaa. Waamoni walitoka wakajipanga kwenye lango la mji, hali wale wafalme waliokuja walikuwa peke yao kwenye tambarare. Yoabu alipoona kuwa vita ni vikali dhidi yake, mbele na nyuma, aliwateua baadhi ya wanajeshi hodari zaidi wa Waisraeli, akawapanga kukabiliana na Waaramu. Wale wanajeshi wengine waliobaki, aliwaweka chini ya uongozi wa Abishai ndugu yake, naye akawapanga ili wakabiliane na Waamoni. Yoabu akamwambia Abishai, “Ikiwa Waaramu wananizidi nguvu, utanisaidia; lakini kama Waamoni wanakuzidi nguvu, nitakuja kukusaidia. Basi jipe moyo! Tupigane kiume kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; na Mwenyezi-Mungu atutendee lile analoona ni jema kwake.” Basi, Yoabu na watu wake walisonga mbele kupigana na Wasiria; nao Waaramu walikimbia. Waamoni walipoona Waaramu wamekimbia, nao walimkimbia Abishai, nduguye Yoabu, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akarudi Yerusalemu. Lakini Waaramu walipoona ya kwamba wameshindwa na Waisraeli, walituma wajumbe waende kuwaleta Waaramu wengine waliokuwa ngambo ya mto Eufrate wakiongozwa na Shofaki, kamanda wa jeshi la Hadadezeri. Daudi alipopata habari, aliwakusanya pamoja Waisraeli wote, akavuka mto Yordani, akawaendea, akapanga vikosi vyake dhidi yao. Daudi alipopanga vita dhidi ya Wasiria, basi nao walipigana naye. Lakini Waaramu walikimbia mbele ya Waisraeli. Daudi aliwaua Waaramu waendeshao magari 7,000 na askari wa miguu 40,000. Pia alimuua Shofaki, kamanda wa jeshi lao. Kisha watumishi wa Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Waisraeli, walifanya mapatano ya amani na Daudi nao wakawa watumishi wa Daudi. Hivyo Waaramu hawakukubali kuwasaidia Waamoni tena. Hata ikawa katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati ambapo wafalme huenda vitani, Yoabu aliliongoza jeshi na kuteka nyara nchi ya Waamoni, pia akaenda na kuuzingira Raba. Lakini Daudi alibaki huko Yerusalemu. Naye Yoabu aliushambulia Raba na kuuharibu; naye Daudi akaichukua taji ya mungu wao Milkomu kichwani pake; naye aligundua ya kwamba taji hiyo ilikuwa na uzito wa kilo thelathini na tano za dhahabu na ndani yake mlikuwemo kito cha thamani. Naye Daudi akakitwaa kupambia taji yake. Pia, aliteka idadi kubwa ya nyara kutoka katika mji huo. Halafu aliwachukua watu wa mji huo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sururu za chuma na mashoka ya chuma. Hivyo ndivyo alivyoitenda miji yote ya Waamoni. Hatimaye Daudi na watu wote wakarudi Yerusalemu. Baada ya hayo, kulitokea vita na Wafilisti huko Gezeri. Sibekai, Mhushathi, akamuua Sipai aliyekuwa mmojawapo wa wazawa wa Warefai; hivyo Wafilisti wakawa wameshindwa. Kulitokea tena vita na Wafilisti. Naye Elhanani mwana wa Yairi alimuua Lahmi nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mpini wa mkuki wake, ulikuwa kama mti wa mfumaji. Baadaye kulitokea tena vita huko Gathi ambako kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na kimo kikubwa, na vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake vidole ishirini na vinne. Yeye pia alikuwa mzawa wa majitu. Naye alipowatukana Waisraeli, Yonathani, mwana wa Shimea, nduguye Daudi, alimuua. Hao walikuwa wazawa wa majitu huko Gathi; nao waliuawa na Daudi pamoja na watumishi wake. Shetani akajitokeza kuwataabisha Waisraeli, akamshawishi Daudii awahesabu watu. Hivyo, Daudi akamwambia Yoabu na wale makamanda wengine, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli, kutoka Beer-sheba mpaka Dani. Nileteeni ripoti ili nijue idadi yao.” Lakini Yoabu akasema, “Mwenyezi-Mungu na awaongeze Waisraeli mara mia kuliko walivyo sasa! Bwana wangu mfalme, kwani hawa wote si watumishi wako? Kwa nini basi unataka kufanya jambo ambalo litawatia Waisraeli katika hatia?” Lakini tamko la mfalme lilikuwa na nguvu zaidi dhidi ya Yoabu. Hivyo, Yoabu akaenda katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu. Yoabu akampelekea mfalme Daudi idadi ya watu: Katika Israeli yote, kulikuwamo wanaume 1,100,000, wenye ujuzi wa kutumia upanga; na katika Yuda kulikuwamo watu 470,000, wenye ujuzi wa kutumia upanga. Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme. Mungu hakupendezwa na jambo hilo kwa hiyo akaiadhibu Israeli. Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa tendo hili nililolifanya! Lakini nakuomba unisamehe mimi mtumishi wako, kwani nimefanya jambo la kipumbavu kabisa.” Basi, Mwenyezi-Mungu alisema na Gadi, mwonaji wa Daudi, akamwambia, “Nenda umwambie Daudi kwamba mimi Mwenyezi-Mungu ninampa mambo matatu. Ajichagulie mojawapo nami nitamtendea.” Hivyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Jichagulie mojawapo: Njaa ya miaka mitatu, au miezi mitatu ya maangamizi kutokana na maadui zako ambapo upanga wa maadui zako utakushinda; au siku tatu ambapo Mwenyezi-Mungu atawashambulia kwa upanga wake, awaletee maradhi mabaya nchini, na malaika wake apite kuwaangamiza katika nchi nzima ya Israeli. Sasa amua, ni jibu lipi nitakalompa yeye aliyenituma.” Daudi akamjibu Gadi, “Nimeingia katika mashaka makubwa! Lakini afadhali niadhibiwe na Mwenyezi-Mungu kwani yeye ana huruma sana. Ila nisianguke katika mkono wa mwanadamu.” Basi, Mwenyezi-Mungu akawaletea Waisraeli maradhi mabaya, ambayo yalisababisha vifo vya Waisraeli 70,000. Halafu Mungu akatuma malaika aende kuuharibu Yerusalemu; lakini kabla hajafanya hivyo, Mwenyezi-Mungu akageuza nia yake na kumwambia malaika huyo aliyetekeleza maangamizi, “Basi, yatosha!” Malaika alikuwa amesimama karibu na uwanja wa kupuria nafaka wa Ornani, Myebusi. Daudi akainua macho yake, akamwona huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama kati ya mbingu na dunia, naye ameunyosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuuangamiza. Hapo Daudi na wazee wote walikuwa wamevaa mavazi ya gunia, wakaanguka kifudifudi. Daudi alimwambia Mungu, “Je, si mimi niliyetoa amri watu wahesabiwe? Ni mimi niliyetenda dhambi na kufanya uovu. Lakini kondoo hawa wamefanya nini? Nakusihi sana, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mkono wako uwe dhidi yangu na dhidi ya jamaa ya baba yangu, lakini maradhi haya mabaya yasiwapate watu wako.” Ndipo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwamuru Gadi amwambie Daudi aende amjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu, katika kiwanja cha kupuria nafaka cha Ornani Myebusi. Daudi akatii amri ya Mwenyezi-Mungu, akapanda juu kufuatana na neno la Gadi alilosema kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Ornani alipogeuka na kumwona yule malaika, ndipo yeye na wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Naye Ornani alikuwa akipura ngano. Daudi alipomwendea Ornani, Ornani alitazama na kumwona Daudi; basi huyo Ornani alitoka kwenye uwanja wa kupuria akaenda mbele; kisha akamsujudia akiinamisha kichwa chake mpaka chini ardhini. Daudi akamwambia Ornani, “Nipe nafasi ya uwanja wako wa kupuria nafaka ili nimjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu juu yake, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa kwa watu. Niuzie kwa bei yake kamili.” Naye Ornani akamwambia Daudi, “Kichukue kiwanja hiki, bwana wangu mfalme, na ukitumie vile unavyopenda mwenyewe. Tazama, nawatoa fahali kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, na vifaa vya kupuria kwa kuni, pamoja na ngano iwe tambiko ya nafaka. Vyote hivyo ninakupa.” Lakini mfalme Daudi alimwambia Ornani, “La, hasha; nitavinunua kwa thamani yake kamili; sitamchukulia Mwenyezi-Mungu kitu kilicho chako au kumtolea tambiko za kuteketezwa ambazo hazijanigharimu kitu.” Hivyo, Daudi alimlipa Ornani kwa kumpimia shekeli 600 kamili za dhahabu kulipia uwanja huo. Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu mahali hapo na kumtolea sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akakubali ombi lake kwa kuleta moto kutoka mbinguni kuiteketeza ile sadaka kwenye madhabahu. Halafu, Mwenyezi-Mungu alimwamuru malaika, naye akaweka upanga wake alani mwake. Wakati huo, Daudi alipoona ya kwamba Mwenyezi-Mungu amekubali ombi lake kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Ornani, Myebusi, akatoa tambiko papo hapo. Hema la Mwenyezi-Mungu ambalo lilitengenezwa na Mose nyikani, na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, wakati huo vilikuwa bado pale mahali pa kuabudia huko Gibeoni. Lakini Daudi hakuweza kwenda huko kumwomba Mungu shauri kwa sababu alikuwa anauogopa upanga wa malaika wa Mwenyezi-Mungu. Basi Daudi akasema, “Hapa ndipo mahali ambapo nyumba ya Mwenyezi-Mungu itakuwa, na hii ndiyo madhabahu ambapo watu wa Israeli watatolea sadaka ya kuteketezwa.” Daudi akatoa amri wageni waliokuwa wanaishi katika nchi ya Israeli wakusanyike, naye akawapangia kazi. Akaweka waashi wachonge vizuri mawe ya kujenga nyumba ya Mungu. Daudi pia akaweka akiba tele ya chuma cha kutengenezea misumari na mafungo ya malango ya nyumba, na akiba tele ya shaba isiyopimika. Mbao za mierezi ambazo Daudi aliletewa na Wasidoni na Watiro zilikuwa hazihesabiki. Daudi akajisemea, “Nyumba ambayo mwanangu Solomoni atamjengea Mwenyezi-Mungu itakuwa ya fahari sana, ya kusifika na tukufu duniani kote. Lakini kwa vile yeye bado angali kijana na bado hana uzoefu mwingi, afadhali nimfanyie matayarisho.” Hivyo basi, Daudi akaweka akiba kubwa sana ya vitu vya ujenzi kabla hajafariki. Ndipo Daudi akamwita Solomoni mwanawe, akamwagiza amjengee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli nyumba. Daudi akamwambia Solomoni, “Mwanangu, nilikusudia moyoni mwangu kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nyumba ili kumtukuza. Lakini Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Wewe umemwaga damu nyingi kwa kupigana vita vikubwa. Kwa sababu ya damu nyingi ambayo umemwaga mbele yangu hapa duniani, hutanijengea nyumba. Hata hivyo, utapata mwana, ambaye atatawala kwa amani kwa sababu nitampa amani na maadui zake wote wa jirani. Jina lake litakuwa Solomoni, kwa maana katika siku za utawala wake, atailetea Israeli amani na utulivu. Hivyo, yeye ndiye atakayenijengea nyumba. Atakuwa mwanangu nami nitakuwa baba yake, na wazawa wake wataitawala Israeli milele.’ Sasa mwanangu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe ili ufaulu kumjengea nyumba kama alivyosema. Mwenyezi-Mungu akupe busara na akili ili atakapokupa uongozi juu ya Israeli, uzishike sheria zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Ukiwa mwangalifu, na ukizitii amri ambazo Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose juu ya Israeli, utastawi. Jipe moyo, uwe imara. Usiogope wala usifadhaike. Kwa juhudi kubwa, nimeiwekea akiba nyumba ya Mwenyezi-Mungu, talanta 100,000 za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha na idadi isiyopimika ya shaba na chuma, kwani ni nyingi sana. Nimeandaa mbao na mawe tayari. Lakini huna budi kuongezea. Unao wafanyakazi wengi: Kuna wachonga mawe, waashi, maseremala na mafundi wa kila aina wenye ujuzi mwingi; wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma. Haya! Anza kazi! Mwenyezi-Mungu na awe pamoja nawe!” Zaidi ya hayo, Daudi aliwaamuru viongozi wote wa Waisraeli wamsaidie Solomoni mwanawe, akisema, “Je, Mwenyezi-Mungu Mungu wenu hayuko pamoja nanyi? Je, hajawapa amani katika pande zote? Yeye aliwatia wakazi wa nchi hii mikononi mwangu na sasa wako chini ya Mwenyezi-Mungu na watu wake. Sasa, mtumikieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa nia na moyo wote. Shime basi! Mjengeeni Mwenyezi-Mungu mahali patakatifu ili sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu pamoja na vyombo vyote vitakatifu vitumiwavyo katika ibada, viwekwe ndani ya nyumba iliyojengwa kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.” Daudi alipokuwa mzee wa miaka mingi, alimtawaza Solomoni mwanawe awe mfalme wa Israeli. Mfalme Daudi aliwakusanya wakuu wote wa Israeli, makuhani na Walawi. Walawi wote wanaume wenye umri wa miaka thelathini na zaidi, wakahesabiwa. Jumla yao ilikuwa 38,000. Hao, Daudi aliwagawanya: 24,000 kati yao wawe wasimamizi wa kazi ya nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu, 6,000 wawe maofisa na waamuzi, 4,000 wawe mabawabu, na 4,000 wawe waimbaji, wakimsifu Mwenyezi-Mungu kwa ala za muziki alizotengeneza mfalme mwenyewe kwa madhumuni hayo. Daudi aliwagawanya Walawi katika makundi matatu kulingana na koo za kabila la Lawi: Ukoo wa Gershoni, ukoo wa Kohathi na ukoo wa Merari. Wana wa Gershoni walikuwa wawili: Ladani na Shimei. Ladani alikuwa na wana watatu: Yehieli mkuu wao, Zethamu na Yoeli. Wana wa Shimei walikuwa watatu: Shelomithi, Hazieli na Harani. Hawa walikuwa viongozi wa ukoo wa Ladani. Wana wa Shimei walikuwa viongozi wanne: Yahathi, Zina, Yeushi na Beria. Yahathi ndiye aliyekuwa mkuu wao, akifuatiwa na Ziza. Lakini Yeushi na Beria, kwa vile hawakuwa na wana wengi, walichukuliwa na ukoo mmoja. Wana wa Kohathi walikuwa wanne: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli. Wana wa Amramu walikuwa Aroni na Mose. Aroni aliteuliwa awe akiweka wakfu vyombo vitakatifu kabisa, pia wazawa wake daima wafukizie ubani mbele za Mwenyezi-Mungu, wakimtumikia na kuwabariki watu katika jina la Mwenyezi-Mungu milele. Lakini wana wa Mose, mtu wa Mungu, hutajwa miongoni mwa kabila la Lawi. Wana wa Mose walikuwa Gershomu na Eliezeri. Aliyekuwa mkuu miongoni mwa wana wa Gershomu ni Shebueli. Eliezeri alikuwa na mwana mmoja tu; Rehabia, naye alikuwa kiongozi. Lakini Rehabia alikuwa na wana wengi sana. Ishari alimzaa Shelomithi, kiongozi wa kabila zima. Wana wa Hebroni walikuwa wanne: Mkuu wao alikuwa Yeria, wa pili Amaria, wa tatu Yahazieli na wa nne Yekameamu. Wana wa Uzieli walikuwa wawili: Mika mkuu wao, na Ishia wa pili. Merari alikuwa na wana wawili: Mali na Mushi. Wana wa Mali walikuwa wawili: Eleazari na Kishi. Eleazari alifariki bila kupata mtoto wa kiume, ila mabinti tu. Mabinti hao waliolewa na binamu zao, wana wa Kishi. Wana wa Mushi walikuwa watatu: Mali, Ederi na Yeremothi. Hao ndio wana wa Lawi kulingana na koo zao. Kila mmoja wao aliyetimiza umri wa miaka ishirini na zaidi, aliandikishwa kwa jina, na alishiriki katika huduma ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Daudi alisema, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, amewapa watu wake amani, naye ataishi Yerusalemu milele. Kwa hiyo, Walawi hawatahitaji tena kulibeba hema takatifu au vyombo vyake vya ibada.” Kulingana na maagizo ya mwisho aliyotoa Daudi, Walawi wote waliofikia umri wa miaka ishirini waliandikishwa. Lakini wajibu wao ulikuwa ni kuwasaidia makuhani wa ukoo wa Aroni katika huduma ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu; kuzitunza nyua na vyumba, kuvisafisha vyombo vitakatifu vyote na kufanya kazi zinazohusu huduma ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Pamoja na hayo, walisaidia katika kazi ya mikate mitakatifu, unga mwembamba na sadaka ya nafaka, maandazi yasiyotiwa chachu, sadaka iliyookwa; sadaka iliyochanganywa na mafuta; pia sadaka katika kazi ya upimaji wa wingi wa sadaka na ukubwa wake na walisimama kumshukuru na kumsifu Mwenyezi-Mungu kila siku asubuhi na jioni, na wakati wa siku za Sabato, mwezi mwandamo na sikukuu, hapo sadaka za kuteketezwa zilipotolewa kwa Mwenyezi-Mungu. Sheria ziliwekwa kuhusu idadi ya Walawi walioagizwa kufanya kazi hizo daima mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kwa hiyo, ulikuwa ni wajibu wao kutunza hema la mkutano na mahali patakatifu, na kuwasaidia ndugu zao makuhani, wazawa wa Aroni, kwenye ibada katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hayo ndiyo makundi ya wazawa wa Aroni. Aroni alikuwa na wana wanne: Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari. Nadabu na Abihu walikufa kabla ya baba yao, wala hawakuwa na watoto; kwa hiyo ndugu zao Eleazari na Ithamari wakawa makuhani. Mfalme Daudi aliwapanga wazawa wa Aroni katika makundi kufuatana na huduma zao. Alisaidiwa kufanya hivyo na Sadoki, mzawa wa Eleazari, na Ahimeleki, mzawa wa Ithamari. Kwa vile ambavyo kulipatikana viongozi wanaume wengi zaidi miongoni mwa wazawa wa Ithamari, waliwagawanya wazawa wa Eleazari chini ya viongozi kumi na sita, na wazawa wa Ithamari chini ya viongozi wanane. Waligawanywa kwa kura kwani kulikuwa na wakuu wa mahali patakatifu na viongozi wa kidini miongoni mwa koo zote mbili, yaani ukoo wa Eleazari na ukoo wa Ithamari. Naye Shemaya mwana wa Nathaneli, mwandishi, aliyekuwa Mlawi, aliwaandika mbele ya mfalme Daudi, maofisa wake, kuhani Sadoki, Ahimeleki mwana wa Abiathari na viongozi wa jamaa za makuhani na za Walawi. Ukoo wa Eleazari ulipata kura mbili, na ukoo wa Ithamari kura moja. Kura ya 1 ilimwangukia Yoaribu; ya 2 Yedaya; ya 3 Harimu; ya 4 Seorimu; ya 5 Malkia; ya 6 Miyamini; ya 7 Hakosi; ya 8 Abiya; ya 9 Yeshua; ya 10 Shekania; ya 11 Eliashibu; ya 12 Yakimu; ya 13 Hupa; ya 14 Yeshebeabu; ya 15 Bilga; ya 16 Imeri; ya 17 Heziri; ya 18 Hapisesi; ya 19 Pethahia; ya 20 Yehezkeli; ya 21 Yakini; ya 22 Gamuli; ya 23 Delaya; na ya 24 Maazia. Hawa waliandikishwa kulingana na kazi zao kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kutoa huduma, kadiri ya utaratibu waliowekewa na Aroni babu yao, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Hawa ndio wazawa wengine wa Lawi: Mmoja wa wazawa wa Amramu alikuwa Shubaeli; wa Shubaeli alikuwa Yedeya. Mmoja wa wazawa wa Rehabia alikuwa Ishio kiongozi wa ukoo. Mmoja wa wazawa wa Ishio alikuwa Shelomithi na wa wazawa wa Shelomithi alikuwa Yahathi. Wana wa Hebroni walikuwa: Yeria wa kwanza, Amaria wa pili, Yahazieli wa tatu, Yakameamu wa nne. Mmoja wa wana wa Uzieli alikuwa Mika. Mmoja wa wazawa wa Mika alikuwa Shamire. Mmoja wa wazawa wa Ishia nduguye Mika alikuwa Zekaria. Wana wa Merari: Mahli, Mushi na Yaazia; wazawa wa Merari kwa mwanawe Yaazia: Shohamu, Zakuri na Ibri. Wana wa Mahli: Eleazari ambaye hakupata mtoto, Kishi ambaye alikuwa na mwana mmoja: Yerameeli. Mushi alikuwa na wana watatu: Mahli, Ederi na Yeremothi. Wao ni wazawa wa Lawi kulingana na koo zao. Pia hao wote walipiga kura kufuatana na ukoo wa kila mkuu na mdogo wake, kama wazawa wa Aroni walivyofanya. Walipiga kura mbele ya mfalme Daudi, Sadoki, Ahimeleki na viongozi wa jamaa za makuhani na za Walawi. Mfalme Daudi na viongozi wa Walawi, waliwateua baadhi ya wana wa Asafu, wa Hemani, na wa Yeduthuni, kuongoza katika huduma ya kutabiri kwa kutumia vinubi, na vinanda na matoazi. Hii ndiyo orodha ya wale waliochaguliwa kuongoza ibada, pamoja na aina ya kazi iliyofanywa na kila kikundi. Wana wanne wa Asafu: Zakuri, Yosefu, Nethania na Asharela. Wao walikuwa chini ya uongozi wa Asafu aliyetabiri wakati wote chini ya uongozi wa mfalme. Wana sita wa Yeduthuni: Gedalia, Seri, Yeshaya, Shimei, Hashabia na Matithia. Wao walikuwa chini ya uongozi wa baba yao; na walitabiri kwa kutumia vinubi, na wakamshukuru na kumtukuza Mwenyezi-Mungu. Wa Hemani: Bukia, Matania, Uzieli, Shebueli, Yeremothi, Hanania, Hanani, Eliatha, Gidalti, Romamti-ezeri, Yoshbekasha, Malothi, Hothiri na Mahaziothi. Mungu alimpa Hemani, mwonaji wa mfalme, hawa watoto wa kiume kumi na wanne, na wa kike watatu, kama alivyoahidi ili kumtukuza. Wanawe wote walipiga muziki kwa matoazi, vinanda na vinubi, kwenye ibada katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakiwa chini ya uongozi wa baba yao. Asafu, Yeduthuni na Hemani walikuwa chini ya amri ya mfalme. Idadi yao pamoja na wale ndugu zao Walawi waliofundishwa kumwimbia Mwenyezi-Mungu, wote waliokuwa stadi, ilikuwa 288. Wote, wakubwa kwa wadogo, waalimu kwa wanafunzi, walitumia kura katika kupanga kazi zao. Kura ya 1 ilimwangukia Yosefu wa jamaa ya Asafu; ya 2 Gedalia pamoja na ndugu zake na wanawe kumi na wawili; ya 3 Zakuri pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 4 ilimwangukia Seri pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 5 Nethania; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 6 Bukia; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 7 Asharela; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 8 Yeshaya; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 9 Matania; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 10 Shimei; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 11 Azareli; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 12 Hashabia; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 13 Shebueli; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 14 Matithia; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 15 Yeremothi; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 16 Hanania; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 17 Yoshbekasha; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 18 Hanani; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 19 Malothi; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 20 Eliatha; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 21 Hothiri; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili; ya 22 Gidalti; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili, ya 23 Mahaziothi; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili, ya 24 ilimwangukia Romamti-ezeri; pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wawili. Haya ndiyo makundi ya Walawi waliofanya kazi za ubawabu. Kutoka katika ukoo wa Kora, alikuwa Meshelemia mwana wa Kore wa jamaa ya Asafu. Yeye alikuwa na wana saba: Zekaria mzaliwa wake wa kwanza, Yediaeli wa pili, Zebadia wa tatu, Yathnieli wa nne, Elamu wa tano, Yohanani wa sita na Eliehoenai wa saba. Pia kulikuwa na Obed-edomu, ambaye Mungu alimbariki kwa kumpa wana wanane: Shemaya mzaliwa wake wa kwanza, Yehozabadi wa pili, Yoa wa tatu, Sakari wa nne, Nethaneli wa tano, Amieli wa sita, Isakari wa saba na Peulethai wa nane. Naye mwanawe Shemaya alipata wana waliokuwa na mamlaka juu ya jamaa ya baba yao, kwa sababu walikuwa wanaume wenye uwezo mkubwa. Shemaya, mzaliwa wa kwanza wa Obed-edomu, alikuwa na wana sita: Othni, Refaeli, Obedi, Elizabadi, nduguze walikuwa mashujaa, Elihu na Semakia. Hao wote wana wa Obed-edomu; wao na wana wao na ndugu zao, walikuwa watu hodari wawezao huo utumishi. Wazawa wote wa Obed-edomu walikuwa sitini na wawili. Naye Meshelemia alikuwa na wana na nduguze; watu wenye uwezo kumi na wanne. Hosa mmojawapo wa wana wa Merari alikuwa na wana wanne: Shimri (aliyefanywa kiongozi na baba yake hata ingawa hakuwa mzaliwa wa kwanza), Hilkia wa pili, Tebalia wa tatu na Zekaria wa nne. Wana wote wa Hosa pamoja na nduguze walikuwa kumi na watatu. Mabawabu hao waligawanyika katika makundi kulingana na jamaa zao, nao pia walipangiwa kazi kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu kama wale Walawi wengine. Kila jamaa, bila kujali wingi, ilipiga kura kuchagua lango watakalosimamia. Kura ya kuchagua wa kulinda lango la mashariki ilimwangukia Shelemia. Walipiga kura pia kwa ajili ya mwanawe Zekaria, aliyekuwa mshauri mwenye busara, ikamwangukia kura ya lango la kaskazini. Obed-edomu aliangukiwa na kura ya lango la kusini, na ya wanawe, ghala. Shupimu na Hosa waliangukiwa na kura ya kulinda lango la magharibi kwenye lango la Shalekethi kwenye barabara ya juu. Ulinzi ulifanywa kwa zamu. Kila siku upande wa mashariki kulikuwa na mabawabu sita, kaskazini wanne, na kusini wanne, pia kwenye ghala kuliwekwa mabawabu wawiliwawili. Kwenye banda zuri lililokuwa upande wa magharibi, kulikuwa na mabawabu wanne barabarani, na wawili kwenye banda lenyewe. Haya ndiyo makundi ya mabawabu miongoni mwa ukoo wa Kora na wazawa wa Merari waliofanya kazi ya ubawabu. Miongoni mwa Walawi, Ahiya alihusika na uangalizi wa hazina ya nyumba ya Mungu, na hazina ya vitu vilivyowekwa wakfu. Ladani, mmoja wa ukoo wa Gershoni, alikuwa babu wa baadhi ya jamaa, miongoni mwao ikiwamo jamaa ya mwanawe Yehieli. Wana wengine wawili wa Ladani, Zethamu na Yoeli, walikuwa watunzaji wa hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Pia kazi ziligawanywa kwa watu wa koo za Wasiria, Waishari, Wahebroni na Wauzieli. Shebueli, mwana wa Gershoni, mwana wa Mose, alikuwa ofisa mkuu wa hazina hizo. Na ndugu yake, alikuwa Eliezeri, aliyekuwa baba yake Rehabia, aliyemzaa Yeshaya, aliyemzaa Yoramu, aliyemzaa Zikri, aliyemzaa Shelomithi. Shelomithi na ndugu zake, ndio waliokuwa waangalizi wa hazina zote za vitu vilivyowekwa wakfu na mfalme Daudi, na viongozi wa jamaa, maofisa wa maelfu na mamia na majemadari wa jeshi. Waliweka wakfu sehemu ya nyara walizoteka vitani kwa ajili ya matengenezo ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Pia, vitu vyote vilivyowekwa wakfu na Samueli, mwonaji, na Shauli mwana wa Kishi, na Abneri, na Yoabu mwana wa Seruya, vilikuwa chini ya uangalizi wa Shelomithi na nduguze. Miongoni mwa Waishari, Kenania na wanawe walipewa kazi za utawala kama maofisa na waamuzi, kwa ajili ya Waisraeli. Miongoni mwa Wahebroni, Hashabia na nduguze 1,700, wote watu mashujaa walipewa wajibu wa kusimamia sehemu za Israeli zilizokuwa upande wa magharibi wa mto Yordani. Walisimamia kazi yote ya Mwenyezi-Mungu na kazi za mfalme Daudi. Miongoni mwa Wahebroni, Yeria alikuwa kiongozi wa koo na jamaa zote, na katika mwaka wa arubaini wa utawala wa mfalme Daudi, uchunguzi ulifanywa, na wanaume wenye uwezo mkubwa walipatikana huko Yezeri katika Gileadi. Mfalme Daudi alimteua Yeriya na ndugu zake 2,700, mashujaa na viongozi wa koo, kusimamia mambo yote yaliyohusu Mungu na mfalme Daudi katika sehemu za Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, zilizokuwa mashariki ya mto Yordani. Hii ndiyo orodha ya wakuu wa wazawa wa Israeli waliokuwa viongozi wa jamaa, na makamanda wa maelfu na mamia na maofisa wao waliomtumikia mfalme Daudi kuhusu zamu za kuingia na kutoka. Kila mwezi kila mwaka, kundi tofauti la watu 24,000 walilishika zamu ya kufanya kazi. Yashobeamu mwana wa Zabdieli alikuwa kiongozi wa kikosi cha kwanza mnamo mwezi wa kwanza; kikosi chake kilikuwa na watu 24,000. Yeye alikuwa mzawa wa Peresi, naye akawa mkuu wa makamanda wote wa jeshi katika mwezi wa kwanza. Dodai alikuwa kiongozi wa kundi la pili katika mwezi wa pili. Kikosi chake kikiwa na wanajeshi 24,000. Kamanda wa kundi la tatu likiwa na wanajeshi 24,000 alikuwa Benaya mwana wa Yehoyada, aliyekuwa kuhani mkuu. Huyu ndiye Benaya aliyekuwa mtu shujaa katika kundi la watu 30, na kiongozi wa kundi hilo. Naye Amizabadi mwanawe, alikuwa kamanda. Asaheli, nduguye Yoabu, alikuwa wa nne akiongoza kundi la nne lenye wanajeshi 24,000, na baada yake alimfuata Zebadia mwanawe. Mwezi wa tano: Shamhuthi, Mwizrahi; alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa sita: Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoa; alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa saba: Helesi, Mpeloni, wa wana wa Efraimu; alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa nane: Sibekai, Mhushathi, wa Wazera; alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa tisa: Abiezeri Mwanathothi, wa Wabenyamini; naye alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa kumi: Maharai, Mnetofathi wa Wazera; naye alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa kumi na moja: Benaya, Mpirathoni; wa wana wa Efraimu, naye alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa kumi na mbili: Heldai, Mnetofathi, wa Othnieli; pia naye alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Hii ndiyo orodha ya wakuu wa makabila ya Israeli: Wa Wareubeni, Eliezeri mwana wa Zikri; Eliezeri ndiye aliyekuwa ofisa mkuu; wa Wasimeoni, Shefatia mwana wa Maaka; wa Lawi, Hashabia mwana wa Kemueli; wa Aroni, Sadoki; wa Yuda, Elihu, mmoja wa ndugu za mfalme Daudi; wa Isakari, Omri mwana wa Mikaeli; wa Zebuluni, Ishmaya mwana wa Obadia; wa Naftali, Yeremothi mwana wa Azrieli; wa wana wa Efraimu, Hoshea mwana wa Azazia; wa nusu ya kabila la Manase, Yoeli mwana wa Pedaya; wa nusu ya kabila la Manase katika Gileadi, Ido mwana wa Zekaria; na wa Benyamini, Yaasieli mwana wa Abneri; wa Dani, Azareli mwana wa Yerohamu. Hao ndio wakuu wa makabila ya Israeli. Mfalme Daudi hakuwahesabu wale waliokuwa chini ya umri wa miaka ishirini kwa maana Mwenyezi-Mungu aliahidi kuwaongeza Waisraeli wawe wengi kama nyota za mbinguni. Yoabu mwana wa Seruya alianza kuwahesabu lakini hakumaliza; tena ghadhabu iliwapata Waisraeli kwa ajili ya tendo hili, nayo hesabu hiyo haikuingizwa katika kumbukumbu za mfalme Daudi. Aliyesimamia hazina za mfalme Daudi alikuwa Azmawethi mwana wa Adieli. Yonathani mwana wa Uzia alisimamia hazina zilizokuwa mashambani, mijini, vijijini na ngomeni. Aliyewasimamia wakulima alikuwa Ezri mwana wa Kelubu. Aliyesimamia kazi ya mashamba ya mizabibu alikuwa Shimei, Mramathi. Aliyesimamia uzalishaji wa divai alikuwa Zabdi, Mshifmi. Aliyesimamia mizabibu na mikuyu ya Shefela alikuwa Baal-hanani, Mgederi. Aliyesimamia ghala za mafuta alikuwa Yoashi. Aliyesimamia mifugo iliyokuwa Sharoni alikuwa Shitrai, Msharoni; aliyesimamia mifugo iliyokuwa mabondeni alikuwa Shafati mwana wa Adlai. Aliyesimamia ngamia alikuwa Obili Mwishmaeli. Aliyesimamia punda alikuwa Yedeya, Mmeronothi. Aliyesimamia makundi ya kondoo alikuwa Yazizi, Mhagri. Hao wote walikuwa watunzaji wa mali ya mfalme Daudi. Yonathani, mjomba wa mfalme Daudi, alikuwa mshauri na mtu mwenye ufahamu na mwandishi. Yeye na Yehieli mwana wa Hakmoni waliwafunza wana wa mfalme. Ahithofeli, alikuwa mshauri wake mfalme; Hushai Mwarki, alikuwa rafiki yake mfalme. Ahithofeli alipofariki, mahali pake palichukuliwa na Yehoyada mwana wa Benaya na Abiathari. Yoabu alikuwa kamanda wa jeshi la mfalme. Mfalme Daudi akawakusanya huko Yerusalemu wakuu wote wa Israeli: Wa makabila, majemadari na vikosi waliomtumikia mfalme, makamanda wa maelfu, makamanda wa mamia, wasimamizi wa mali zote na ng'ombe wote wa mfalme, na wanawe pamoja na maofisa wa ikulu, mashujaa na askari wote mashuhuri. Ndipo mfalme Daudi akasimama akasemana kusema: “Enyi ndugu zangu na watu wangu, nisikilizeni. Nilikusudia moyoni mwangu kujenga nyumba kwa ajili ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, kiti cha kuwekea miguu yake Mungu wetu; na nilifanya maandalizi ya kujenga. Lakini Mungu alinikataza, kwa sababu mimi ni mtu wa vita na nimekwisha mwaga damu nyingi. Lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli alinichagua mimi miongoni mwa jamaa ya baba yangu kuwa mfalme wa Israeli milele. Alilichagua kabila la Yuda liongoze; na kutokana na kabila hilo, aliichagua jamaa ya baba yangu, na miongoni mwa wana wa baba yangu, alipendezwa nami na kuniweka niwe mfalme wa Israeli yote. Mwenyezi-Mungu amenijalia wana wengi, na miongoni mwa hao wote, amemchagua Solomoni mwanangu, aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wake Mwenyezi-Mungu aitawale Israeli. “Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Mwanao Solomoni ndiye atakayenijengea nyumba na nyua zangu, kwa maana nimemchagua yeye awe mwanangu, nami nitakuwa baba yake.’ Nitauimarisha ufalme wake milele ikiwa ataendelea kuzishika kwa dhati amri na sheria zangu kama anavyofanya leo. “Basi sasa, mbele ya kusanyiko hili la Waisraeli wote, jumuiya ya watu wa Mwenyezi-Mungu, na mbele ya Mungu wetu, angalieni mzishike amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili mwendelee kuimiliki nchi hii nzuri, na kuwarithisha wazawa wenu baada yenu, hata milele. “Nawe Solomoni mwanangu, umjue Mungu wa baba yako, na umtumikie kwa moyo wako wote na kwa nia thabiti; yeye Mwenyezi-Mungu huchunguza mioyo na anafahamu mipango na fikira za binadamu. Ukimtafuta yeye, utamwona; lakini ukimwacha, atakutupilia mbali milele. Basi, ujihadhari na kukumbuka ya kwamba, Mwenyezi-Mungu amekuchagua wewe umjengee nyumba ya ibada. Uwe hodari ukatende hivyo.” Ndipo Daudi akampa Solomoni mwanawe ramani ya majengo yote ya hekalu, nyumba zake, hazina zake, ghorofa zake, vyumba vyake vya ndani na mahali pa kiti cha rehema. Alimpa ramani ya yote aliyokusudia moyoni kuhusu nyua za nyumba ya Mwenyezi-Mungu, vyumba vya Mungu na ghala za kuwekea vitu vilivyo wakfu. Alimpa pia mfano wa jinsi ya kuwapanga makuhani na Walawi kuzitekeleza huduma zao, kutumikia nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuvitunza vyombo vyote vya Nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Alimpa kiasi cha dhahabu iliyohitajika kutengenezea vyombo vyote vya dhahabu vya utumishi wa kila namna, kiasi cha fedha iliyohitajika kwa utumishi wa kila namna, uzani wa vinara vya dhahabu na taa zake, uzani wa dhahabu ya kila kinara na taa zake uzani wa fedha ya kutengenezea kinara na taa zake kulingana na matumizi ya kila kinara; na kiasi cha dhahabu ya kutengenezea meza za dhahabu zilizowekewa mikate iliyotolewa kwa Mungu, hata kiasi cha fedha ya kutengenezea meza za fedha; pia alitoa maagizo kuhusu kiasi cha dhahabu safi iliyohitajika kutengenezea nyuma, mabirika na vikombe, pia kiasi cha dhahabu na fedha iliyohitajika kutengenezea mabakuli ya dhahabu na ya fedha, na kiasi cha dhahabu safi ya kutengenezea madhabahu ya kufukizia ubani. Alimpa pia mfano wake wa gari la dhahabu la viumbe wenye mabawa waliyotandaza mabawa na kulifunika sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Hayo yote, mfalme Daudi aliyaweka wazi kwa maandishi aliyopewa na Mwenyezi-Mungu. Kazi yote itendeke kulingana na ramani hiyo. Kisha, mfalme Daudi akamwambia Solomoni mwanawe, “Uwe imara na hodari, uifanye kazi hii. Usiogope wala kuwa na wasiwasi. Mungu, Mwenyezi-Mungu ambaye ni Mungu wangu, yu pamoja nawe. Hatakuacha bali atakuwa nawe hata itakapomalizika kazi yote inayohitajika kufanyiwa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Makuhani na Walawi wamekwisha pangiwa kazi watakazofanya katika nyumba ya Mungu. Wafanyakazi wenye ujuzi wa kila aina watakuwa tayari kabisa kukusaidia, na watu wote pamoja na viongozi wao watakuwa chini ya amri yako.” Mfalme Daudi akaumbia ule mkutano wote uliojumuika, “Solomoni, mwanangu, ambaye peke yake amechaguliwa na Mungu, bado yungali mdogo, na hana uzoefu mwingi, na kazi hii ni kubwa. Nyumba atakayoijenga si ya mwanadamu, bali ni ya Mungu, Mwenyezi-Mungu. Basi, nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu wote kuiwekea nyumba ya Mungu wangu, akiba ya dhahabu ya kutengenezea vitu vya dhahabu, fedha ya kutengenezea vitu vya fedha, shaba ya kutengenezea vitu vya shaba, chuma cha kutengenezea vitu vya chuma, na miti ya kutengenezea vitu vya miti. Zaidi ya hayo, nimevitayarisha kwa wingi vito vya rangi na mawe ya kujazia vito vya njumu, mawe ya rangi, mawe ya thamani ya kila namna na marumaru. Tena, zaidi ya vyote nilivyotoa kwa ajili ya nyumba takatifu, ninayo hazina yangu binafsi ya dhahabu na fedha, na kwa sababu naipenda nyumba ya Mungu wangu, naitoa kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu: Tani 3,000 za dhahabu kutoka Ofiri, talanta 700 za fedha safi ya kuzifunikia kuta za nyumba, na kwa ajili ya kutengenezea vitu vya kila aina vitakavyotengenezwa na mafundi kwa mikono. Nimeweka dhahabu kwa ajili ya vyombo vya dhahabu, na fedha kwa ajili ya vyombo vya fedha. Ni nani basi atakayemtolea Mwenyezi-Mungu kwa hiari ili ajiweke wakfu hivi leo kwa Mwenyezi-Mungu?” Ndipo wakuu wa koo, viongozi wa makabila ya Israeli, makamanda wa maelfu na wa mamia; pia na maofisa wasimamizi wa kazi za mfalme walipotoa kwa hiari yao. Walitoa kwa ajili ya huduma za nyumba ya Mungu: Tani 170 za dhahabu, tani 340 za fedha, tani 620 za shaba na tani 3,400 za chuma. Wale ambao walikuwa na vito vya thamani walivitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, chini ya uangalizi wa Yehieli, Mgershoni. Ndipo watu wakafurahi kwa sababu walitoa kwa hiari, maana kwa moyo wao wote walimtolea Mwenyezi-Mungu kwa hiari, naye mfalme Daudi alifurahi sana. Ndipo Daudi akamtukuza Mwenyezi-Mungu mbele ya mkutano wote, akisema: “Utukuzwe milele na milele, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yetu Israeli. Ukuu ni wako, ee Mwenyezi-Mungu, una nguvu, utukufu, ushindi na enzi. Vyote vilivyoko mbinguni na duniani ni vyako. Ee Mwenyezi-Mungu, ufalme ni wako, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako, vyote wavitawala. Uwezo na nguvu vimo mkononi mwako, nawe wawakuza uwapendao, na huwaimarisha wote. Sasa ee Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. “Lakini, mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kukupa kitu? Kwa maana vitu vyote vyatoka kwako, tumekutolea vilivyo vyako wewe mwenyewe. Sisi tu wageni mbele yako, na wasafiri kama walivyokuwa babu zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli kipitacho, hapa hakuna tumaini la kukaa. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wingi wote huu tuliotoa ili kukujengea nyumba kwa ajili ya utukufu wa jina lako takatifu, watoka mkononi mwako na yote ni yako. Ninajua Mungu wangu, kwamba wewe waujaribu moyo, nawe unapendezwa na unyofu. Nami, katika unyofu wa moyo wangu nimetoa vitu hivi vyote kwa hiari yangu, na sasa ninaona watu wako walioko hapa, wakikutolea kwa hiari na furaha. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, babu zetu, dumisha maazimio ya namna hiyo na fikira za namna hiyo mioyoni mwa watu wako, na ielekeze mioyo ya watu wako kwako. Mjalie Solomoni mwanangu ili kwa moyo wote ashike amri zako, maamuzi na maagizo yako, atekeleze yote ili aweze kuijenga nyumba hii ya enzi niliyoifanyia matayarisho.” Kisha, mfalme Daudi aliwaambia wote waliokusanyika, “Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Na wote waliokusanyika wakamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, wakamsujudia na kumwabudu Mwenyezi-Mungu na kumtolea mfalme Daudi heshima. Wakamtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Siku ya pili yake wakamtolea sadaka za kuteketezwa: Mafahali 1,000, wanakondoo 1,000, pamoja na sadaka zao za vinywaji na tambiko nyingi kwa ajili ya Waisraeli wote. Basi siku hiyo walikula na kunywa kwa furaha kuu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Wakamtawaza Solomoni mwana wa Daudi, mara ya pili. Wakampaka mafuta awe mtawala kwa jina la Mwenyezi-Mungu, na Sadoki awe kuhani. Ndipo Solomoni akaketi katika kiti cha enzi cha Mwenyezi-Mungu, badala ya Daudi baba yake. Naye akafanikiwa, na taifa lote la Israeli likamtii. Viongozi wote, mashujaa na wana wote wa Daudi wakajiweka chini ya mfalme Solomoni. Mwenyezi-Mungu akampa Solomoni sifa nzuri machoni pa Waisraeli wote, akampa fahari ya kifalme ipitayo fahari ya mfalme awaye yote aliyeitawala Israeli kabla yake. Basi Daudi, mwana wa Yese, akawa mfalme juu ya Israeli yote. Na muda aliotawala juu ya Israeli ulikuwa miaka arubaini; miaka saba alitawala huko Hebroni na miaka thelathini na mitatu alitawala huko Yerusalemu. Alikufa akiwa mzee mwenye miaka mingi, ameshiba siku, akiwa na mali na heshima. Solomoni mwanawe, akawa mfalme badala yake. Habari za mfalme Daudi toka mwanzo hadi mwisho, zimeandikwa katika kumbukumbu za Samueli mwonaji, katika kumbukumbu za nabii Nathani na katika kumbukumbu za Gadi mwonaji. Hizo zasema pamoja na mambo ya utawala wake, uwezo wake, na mambo yaliyompata yeye, Waisraeli, na falme zote nchini. Solomoni, mwanawe mfalme Daudi, alijiimarisha katika utawala wake, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wake alikuwa pamoja naye, akambariki na kumfanya awe mkuu sana. Mfalme Solomoni aliwaita makamanda wote wa vikosi vya maelfu na vya mamia, waamuzi, na viongozi wote wa koo za Israeli. Kisha akaandamana nao hadi mahali pa ibada huko Gibeoni. Walikwenda huko kwa sababu hapo ndipo mahali lilipokuwa hema la mkutano la Mungu alilolitengeneza Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, nyikani. (Lakini, sanduku la Mungu lilikuwa Yerusalemu katika hema ambalo mfalme Daudi alilipigilia alipolileta kutoka Kiriath-yearimu). Tena, madhabahu ya shaba iliyotengenezwa na Bezaleli, mwana wa Uri na mjukuu wa Huri, pia ilikuwa huko Gibeoni mbele ya hema takatifu la Mwenyezi-Mungu. Hapo mfalme Solomoni na watu wote wakamwomba Mwenyezi-Mungu. Solomoni alipanda mbele ya madhabahu ya shaba iliyokuwa kwenye hema la mkutano. Hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akatoa tambiko 1,000 za kuteketezwa juu ya madhabahu hayo. Usiku huo, Mungu alimtokea Solomoni, akamwambia, “Omba chochote, nami nitakupa.” Solomoni akamwambia Mungu, “Ulimwonesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, na umenijalia kuwa mfalme mahali pake. Sasa, ee Mungu, Mwenyezi-Mungu, itimize ahadi uliyompa baba yangu Daudi. Umenitawaza niwe mfalme juu ya watu hawa walio wengi kama mavumbi. Kwa hiyo, nakuomba unipe hekima na maarifa ili niweze kuwatawala watu wako vizuri. La sivyo, nitawezaje kuwatawala hawa watu wako walio wengi hivi?” Mungu akamjibu Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili uliloomba limo moyoni mwako, na wala hukuomba mali, wala utajiri, wala heshima wala hukuomba wanaokuchukia waangamizwe, wala maisha marefu, lakini umeomba hekima na maarifa ili uwatawale vizuri watu wangu ambao nimekupa uwe mfalme wao, ninakupa hekima na maarifa. Pia, nitakupa utajiri, mali na heshima zaidi ya mfalme mwingine yeyote aliyekuwako kabla yako na mfalme mwingine yeyote atakayetawala baada yako.” Basi, Solomoni aliondoka mahali hapo pa kuabudia, huko Gibeoni, lilipokuwa hema la mkutano, akarudi Yerusalemu. Akaitawala Israeli. Solomoni alikusanya magari ya farasi na wapandafarasi; alikuwa na magari ya farasi 1,400, na wapandafarasi 12,000, ambao aliwaweka katika miji yenye vituo vya magari ya farasi na kwake katika Yerusalemu. Mfalme Solomoni aliongeza fedha na dhahabu zikawa nyingi kama mawe katika Yerusalemu, na mbao za mierezi zikapatikana kwa wingi kama mikuyu ya Shefela. Farasi wa Solomoni walitoka Misri na Kilikia; wafanyabiashara wake waliwanunua huko. Walinunua gari moja la farasi kutoka Misri kwa bei ya shekeli 600 za fedha, na farasi mmoja kwa shekeli 150 za fedha. Kisha waliwauzia wafalme wa Wahiti na Shamu farasi hao na magari. Mfalme Solomoni alikata shauri kujenga nyumba ambamo Mwenyezi-Mungu ataabudiwa, na pia kujijengea yeye mwenyewe jumba la kifalme. Alipanga wanaume 70,000 wawe wachukuzi wa mizigo, 80,000 wawe wachonga mawe milimani na wengine 3,600 wawe wasimamizi wao. Kisha, Solomoni akatuma ujumbe kwa Hiramu, mfalme wa Tiro, akamwambia, “Nitendee na mimi kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, ulipompelekea mierezi ya kujengea ikulu. Tazama, karibu nianze kujenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Nitaiweka wakfu, nayo itakuwa mahali pa kufukiza ubani wa harufu nzuri mbele yake, na mahali pa mikate ya kuwekwa mbele yake daima, na tambiko za kuteketezwa asubuhi na jioni na pia siku za Sabato, mwezi mwandamo, na sikukuu nyinginezo za Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama alivyoiagiza Israeli milele. Nyumba ninayokusudia kujenga itakuwa kubwa sana, kwani Mungu wetu ni mkuu zaidi ya miungu yote. Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba ikiwa mbingu zenyewe hazimtoshi, wala mbingu za juu sana? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba isipokuwa tu kama mahali pa kufukizia ubani mbele yake? Basi, sasa nitumie mtu mwenye ujuzi wa kutengeneza vyombo kwa dhahabu, fedha, shaba, na chuma, na nguo za rangi ya zambarau, za rangi nyekundu na ya samawati, ajuaye pia, kutia nakshi. Yeye atashirikiana katika kazi hiyo na mafundi walioko pamoja nami katika Yuda na Yerusalemu, ambao baba yangu Daudi aliwachagua. Tena nipelekee mierezi, miberoshi na misandali kutoka Lebanoni, kwa maana najua ya kwamba watumishi wako ni hodari sana wa kupasua mbao huko Lebanoni. Nao watumishi wangu watashirikiana na watumishi wako, ili wanipasulie mbao kwa wingi, maana nyumba ninayokusudia kujenga ni kubwa na ya ajabu. Kwa ajili ya watumishi wako, yaani maseremala watakaopasua mbao, nitatoa tani 2,000 za ngano iliyopondwa, tani 2,000 za shayiri, lita 400,000 za divai na lita 400,000 za mafuta.” Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, alimjibu Solomoni kwa barua akisema: “Kwa kuwa Mwenyezi-Mungu anawapenda watu wake, amekufanya uwe mfalme wao. Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliyeziumba mbingu na dunia! Amempa mfalme Daudi mwana mwenye hekima, busara na akili, atakayemjengea Mwenyezi-Mungu nyumba, na kujijengea ikulu. Sasa nakupelekea fundi stadi sana na mwenye akili, jina lake Huramu-abi, mwana wa mmoja wa wanawake wa kabila la Dani, na baba yake alikuwa mkazi wa Tiro. Yeye ana ujuzi mwingi wa kutumia dhahabu, fedha, shaba, chuma, mawe, miti, rangi ya zambarau, ya samawati, nyekundu na nguo za kitani safi. Tena ni hodari na anaweza kutia nakshi na kuchora michoro ya kila aina kufuatana na kielelezo chochote ambacho angepewa. Yeye atafanya kazi pamoja na mafundi wako, mafundi wa bwana wangu, Daudi, baba yako. Sasa basi, bwana wangu, vitu hivyo ulivyosema: Ngano, shayiri, mafuta na divai, tafadhali uvitume kwa watumishi wako, nasi tutapasua mbao kadiri ya mahitaji yako kutoka huko Lebanoni; kisha tutazifunga pamoja zielee majini mpaka Yopa. Kutoka huko utazipeleka Yerusalemu.” Mfalme Solomoni aliamuru sensa ifanywe ya wageni wote walioishi katika nchi ya Israeli. Sensa hii ni kama ile aliyoifanya Daudi, baba yake. Kulikuwa na wageni wapatao 153,600. Kati yao, 70,000 aliwapa kazi ya upagazi, 80,000 wakawa wachonga mawe milimani, na 3,600 wakawa wasimamizi ili wawahimize watu kufanya kazi. Kisha Solomoni alianza kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu katika Yerusalemu juu ya mlima Moria ambapo Mwenyezi-Mungu alimtokea Daudi baba yake, mahali ambapo Daudi alikuwa amepachagua, kwenye kiwanja cha kupuria cha Ornani Myebusi. Mfalme Solomoni alianza ujenzi wa hekalu mnamo mwezi wa pili wa mwaka wa nne wa utawala wake. Vipimo alivyotumia Solomoni katika ujenzi wa nyumba ya Mungu, vilikuwa kadiri ya vipimo vya awali, urefu mita 27 na upana mita 9. Chumba cha sehemu ya kuingilia kilikuwa na urefu wa mita 9, sawa na upana wa nyumba hiyo, na kimo chake mita 54. Kuta zake zilifunikwa kwa dhahabu safi upande wa ndani. Ukumbi ulizungushiwa mbao za miberoshi na kufunikwa kwa dhahabu safi na kuchorwa mifano ya miti ya mitende na minyororo. Mfalme Solomoni aliipamba nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa mawe mazuri ya thamani. Dhahabu aliyotumia ilitoka nchi ya Parvaimu. Aliifunika nyumba yote kwa dhahabu: Boriti zake, vizingiti vyake, kuta zake na milango yake. Kutani palichongwa viumbe wenye mabawa. Tena, alipatengeneza mahali patakatifu sana. Urefu wake ulikuwa mita 9, sawasawa na upana wake ambao pia ulikuwa mita 9. Alitumia zaidi ya tani 20 za dhahabu kukifunika chumba hicho. Misumari aliyoitumia ilikuwa ya uzani wa gramu 570 za dhahabu. Pia alivifunika vyumba vyote vya ghorofani kwa dhahabu. Alitengeneza sanamu mbili za viumbe wenye mabawa kwa mbao, akazifunika kwa dhahabu na kuziweka mahali patakatifu sana. Kila kiumbe kilikuwa na mabawa mawili yenye urefu wa mita 4.4 jumla, mita 2.25 kila bawa. Bawa mojawapo liligusa ukuta upande mmoja wa chumba na la pili liligusana na la kiumbe wa pili. Kadhalika bawa moja la kiumbe wa pili liligusa ukuta upande mwingine wa chumba na la pili likagusana na la kiumbe wa kwanza katikati ya chumba. Urefu wa mabawa mawili ya viumbe hawa ni mita 4.5. Yalisimama sambamba, nyuso za viumbe wenye mabawa zikielekea ukumbini. Alitengeneza pazia kwa kitambaa cha kitani safi, cha rangi ya samawati, ya zambarau na nyekundu. Alilinakshi kwa michoro ya viumbe wenye mabawa. Mfalme Solomoni alitengeneza nguzo mbili za shaba, kila moja yenye urefu wa mita 15.5, akaziweka mbele ya nyumba. Kila nguzo ilikuwa na taji juu yake yenye urefu wa mita 2.2. Alitengeneza namna ya mapambo ya mikufu juu ya vichwa vya nguzo hizo, akachonga pia michoro ya makomamaga 100 juu yake. Alizisimamisha nguzo hizo kwenye sebule ya hekalu, moja upande wa kusini, na nyingine upande wa kaskazini; ile ya upande wa kusini aliita Yakini, na ya upande wa kaskazini akaiita Boazi. Mfalme Solomoni alitengeneza madhabahu ya shaba ya mraba mita 9 kwa mita 9, na kimo chake mita 4.5. Kisha, alitengeneza tangi la maji la mviringo, lenye upana wa mita 4.5 kutoka ukingo hadi ukingo, kina cha mita 2.25, na mzingo wa mita 13.5. Chini ya ukingo kulizunguka hilo tangi, kulikuwa na safu mbili za mapambo ya mafahali, safu moja juu ya safu nyingine; mapambo hayo yalifyatuliwa pamoja na sehemu nyingine za hilo tangi. Nalo tangi lilikuwa limewekwa juu ya sanamu za mafahali kumi na wawili, tatu zikielekea kaskazini, tatu magharibi, tatu kusini na nyingine tatu mashariki. Unene wa ukingo wake ulikuwa sentimita 7.5. Ukingo wake ulikuwa kama ukingo wa kikombe, na kama ua la yungiyungi. Tangi hilo liliweza kuchukua kiasi cha lita 60,000 za maji. Alitengeneza pia birika kumi za kuoshea vitu vilivyotumika katika tambiko za kuteketezwa. Tano kati ya bakuli hizo aliziweka kusini na tano upande wa kaskazini. Tangi lilitumiwa na makuhani kunawia. Alitengeneza vinara kumi vya dhahabu kama ilivyoagizwa, akaviweka ukumbini mwa hekalu; vitano upande wa kusini, na vitano upande wa kaskazini. Alitengeneza pia meza kumi, nazo akaziweka ukumbini mwa hekalu. Kisha alitengeneza birika 100 za dhahabu. Alitengeneza ua wa ndani wa makuhani na mwingine mkubwa wa nje, na milango ya ua ambayo aliifunika kwa shaba; na lile tangi akaliweka kwenye pembe ya kusini-mashariki ya nyumba. Huramu alitengeneza vyungu, sepetu na mabirika. Basi Huramu akamaliza kazi aliyomfanyia mfalme Solomoni kuhusu nyumba ya Mungu: Nguzo mbili, mabakuli, taji mbili juu ya nguzo, na nyavu mbili kwa ajili ya kufunika mabakuli ya taji zilizowekwa juu ya nguzo; pia mifano ya makomamanga 400 kwa ajili ya nyavu hizo mbili, safu mbilimbili za makomamanga kwa kila wavu, ili kupamba mabakuli yale mawili ya taji zilizokuwa juu ya kila nguzo. Hali kadhalika alitengeneza birika juu ya magari, na tangi lile moja, na sanamu za mafahali kumi na mawili chini ya hilo tangi. Halafu masufuria, sepetu na nyuma na vyombo vingine vyote vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambavyo Huramu-abi alimtengenezea mfalme Solomoni, vilikuwa vya shaba iliyongarishwa. Vitu hivyo vyote mfalme alivitengeneza katika uwanda wa Yordani, sehemu ya udongo wa mfinyanzi iliyokuwa kati ya Sukothi na Sereda. Uzani wa shaba iliyotumika kutengenezea vyombo hivi haukujulikana kwa maana Solomoni alitengeneza vyombo vingi sana. Solomoni alitengeneza vitu vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mungu: Madhabahu ya dhahabu na meza za mikate ya kuwekwa mbele ya Mungu; vinara na taa za dhahabu safi za kuangazia mahali pale patakatifu sana, kama ilivyoamriwa; maua, taa na koleo, vyote vikiwa vya dhahabu safi kabisa; mikasi na mabirika, visahani vya ubani na vyetezo vya kubebea moto, vyote vya dhahabu safi. Pete za hekalu za milango ya mahali pale patakatifu sana, na za milango mingine ya ukumbi, zote zilitengenezwa kwa dhahabu. Hivyo, Solomoni akamaliza kazi zote zilizohusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kisha Solomoni akaleta mali yote Daudi baba yake aliyokuwa ameiweka wakfu, yaani: Fedha, dhahabu na vyombo; akaiweka katika hazina za nyumba ya Mungu. Basi mfalme Solomoni akawakutanisha Yerusalemu wazee na viongozi wote wa makabila na wa koo za Israeli ili waliondoe sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu kutoka katika mji wa Daudi, yaani Siyoni. Ndipo wote walipokutana mbele ya mfalme katika sikukuu ya mwezi wa saba. Baada ya wazee wote wa Israeli kuwasili, Walawi walilibeba sanduku la agano, Walawi na makuhani walilihamisha sanduku la agano na hema la mkutano na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa humo hemani. Mfalme Solomoni na mkutano wa Israeli wakakusanyika mbele ya sanduku la agano nao wakatoa sadaka za ng'ombe na kondoo wasiohesabika. Kisha makuhani wakaliingiza sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu mahali pake, katika chumba cha ndani cha nyumba, mahali patakatifu sana, chini ya mabawa ya wale viumbe. Hao viumbe wenye mabawa walitandaza mabawa yao juu ya mahali lilipowekwa sanduku, kwa hiyo sanduku na mipiko yake ya kulibebea vilikuwa chini ya mabawa. Kwa kuwa mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana, ncha zake ziliweza kuonekana kutoka mahali patakatifu mbele ya chumba cha ndani, lakini haikuweza kuonekana kutoka upande wa nje. Mipiko hiyo ingali mahali hapo hata leo. Hakukuwa na kitu ndani ya sanduku la agano, ila vile vibao viwili vya mawe ambavyo Mose aliviweka humo kule Horebu, mahali Mwenyezi-Mungu alipofanya agano na watu wa Israeli, walipotoka Misri. Ikawa makuhani walipotoka pale mahali patakatifu, (kwa sababu makuhani wote waliokuwapo bila kujali makundi yao, walikuwa wamejitakasa.), Walawi wote waimbaji, wakiwamo Asafu, Hemani, na Yeduthuni, pamoja na Walawi wengine wa koo zao, wakiwa wamejivalia nguo zao za kitani safi huku wamebeba matoazi, vinanda na vinubi, walisimama upande wa mashariki wa madhabahu. Makuhani 120 wapiga tarumbeta walikuwa pamoja nao. Waimbaji, huku wakifuatiwa na sauti linganifu za tarumbeta, matoazi na vyombo vingine vya muziki, walimsifu Mwenyezi-Mungu wakiimba: “Maana yeye ni mwema, na fadhili zake zadumu milele.” Wakati huo nyumba ya Mwenyezi-Mungu ilijazwa wingu. Nao makuhani walishindwa kuhudumu humo kwa sababu ya wingu hilo, maana utukufu wa Mwenyezi-Mungu uliijaza nyumba ya Mungu. Ndipo Solomoni akasema, “Mwenyezi-Mungu alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Hakika nimekujengea nyumba tukufu, mahali pa makao yako ya milele.” Kisha Solomoni akaigeukia jumuiya yote ya watu wa Israeli wakiwa wamesimama, akawabariki. Akasema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwani kwa nguvu yake ameitimiza ahadi yake aliyoitoa kwa baba yangu Daudi akisema, ‘Tangu niwaondoe watu wangu kutoka nchi ya Misri, sikuchagua mji wowote katika makabila ya Israeli ili nijengewe nyumba nitakamoabudiwa; na sikumchagua mtu yeyote awe mkuu wa watu wangu Israeli. Nimeuchagua mji wa Yerusalemu uwe mji ambamo nitaabudiwa, na nimemchagua Daudi awatawale watu wangu Israeli.’ “Kwa hiyo, baba yangu Daudi alikusudia kujenga nyumba atakamoabudiwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia baba yangu Daudi, ‘Ni vyema kwamba ulikusudia moyoni mwako kunijengea nyumba. Hata hivyo, si wewe utakayejenga hiyo nyumba, ila mwanao utakayemzaa ndiye atakayenijengea hiyo nyumba.’” “Na sasa Mwenyezi-Mungu ametimiza ahadi yake, kwani nimekuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, na kukikalia kiti cha enzi cha Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyoahidi; pia nimejenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Katika nyumba hiyo nimeliweka sanduku la agano, ambalo ndani yake mna agano la Mwenyezi-Mungu alilofanya na watu wa Israeli.” Kisha, Solomoni alisimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu halafu mbele ya jumuiya yote ya watu wa Israeli, aliinua mikono yake juu. Solomoni alikuwa ametengeneza jukwaa la shaba ambalo aliliweka katikati ya ua. Urefu na upana wake ulikuwa mita mbili na robo, na kimo chake mita moja na robo. Alipanda jukwaani na kupiga magoti mbele ya jumuiya yote ya Israeli, akainua mikono yake kuelekea mbinguni. Aliomba akisema, “Ee, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu mwingine kama wewe, mbinguni ama duniani. Wewe ni mwaminifu, kwani umetimiza agano lako na kuwaonesha fadhili zako watumishi wako wanaoishi wakikutii kwa moyo wao wote. Umetimiza ahadi uliyotoa kwa mtumishi wako baba yangu Daudi; naam, yale uliyonena umeyatimiza leo kwa uwezo wako mwenyewe. “Kwa hiyo sasa, Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninakuomba pia utimize ile ahadi uliyomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu, ukisema, ‘Siku zote utakuwa na mzawa wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, iwapo wazawa wako watafuata kwa uangalifu sheria yangu kama wewe ulivyofanya mbele yangu.’ Sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakusihi utimize yote uliyomwahidi mtumishi wako Daudi. “Lakini, ee Mungu kweli utakaa humu duniani na binadamu? Hata mbingu zenyewe, wala mbingu za mbingu za juu sana hazikutoshi, itakutoshaje nyumba hii ambayo nimeijenga? Hata hivyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mimi mtumishi wako, nakuomba unisikilize na kunitimizia ombi langu ninalokuomba leo. Ichunge nyumba hii mchana na usiku, mahali ambapo umechagua watu wako waliabudu jina lako. Unisikie mimi mtumishi wako ninapokuja mahali hapa kuomba. Sikia maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watu wako Israeli wanapoomba wakielekea mahali hapa. Usikie maombi kutoka huko mbinguni na ukisha sikia, utusamehe. “Mtu akimkosea mwenzake, naye akaletwa apate kuapa mbele ya madhabahu yako katika nyumba hii, na akiapa tafadhali wewe usikie kutoka huko mbinguni, uchukue hatua na kuwahukumu watumishi wako. Aliye na hatia umwadhibu kadiri ya makosa yake; asiye na hatia umwachilie na kumpatia tuzo kadiri ya uadilifu wake. “Wakati watu wako Israeli watakaposhindwa na maadui zao, kwa sababu ya dhambi walizotenda dhidi yako, nao wakitubu kwako na kukiri jina lako, wakiomba msamaha wako kwa unyenyekevu katika nyumba hii, basi, usikie kutoka huko mbinguni. Usamehe dhambi zao na uwarudishe katika nchi uliyowapa wao na babu zao. “Mvua isiponyesha kwa sababu wametenda dhambi dhidi yako, wakiomba wakielekea mahali hapa na kulikiri jina lako, pia wakiziacha dhambi zao, tafadhali uwasikie kutoka huko mbinguni, na usamehe dhambi zao watumishi wako watu wako Waisraeli, huku ukiwafundisha kufuata njia nyofu, ukanyeshe mvua katika nchi yako hii ambayo uliwapa watu wako iwe mali yao. “Iwapo kuna njaa nchini au tauni, ukame, ugonjwa wa mimea, nzige au viwavi, au ikiwa watu wako wamezingirwa na maadui zao katika mji wao wowote ule; ikiwa kuna pigo lolote au ugonjwa wowote, tafadhali usikie maombi yoyote yatakayoombwa na mtu yeyote au watu wako wote wa Israeli, kila mtu akijua taabu yake na huzuni yake akikuomba huku akinyosha mikono yake kuelekea nyumba hii. Basi usikie kutoka kwako mbinguni, utoe msamaha, pia umtendee kila mtu kadiri anavyostahili, kwani ni wewe tu ujuaye mawazo ya mioyo ya wanadamu wote. Hivyo watakutii na kuenenda katika njia zako wakati wote wanapoishi katika nchi uliyowapa babu zetu. “Vivyo hivyo wakati mgeni asiye mmoja wa watu wako Israeli atakuja kutoka nchi ya mbali kwa ajili ya jina lako kuu, na kwa sababu ya nguvu na ulinzi wako, kuomba katika nyumba hii, nakusihi umsikie toka huko kwako mbinguni, na umjalie huyo mgeni yote atakayokuomba kusudi watu wote ulimwenguni wapate kujua jina lako na kukutii kama wafanyavyo watu wako Israeli na wapate kufahamu kwamba nyumba hii ambayo nimeijenga inajulikana kwa jina lako. “Watu wako wakienda vitani kupigana na maadui zao kokote kule utakakowapeleka, nao wakikuomba wakielekea mji huu uliouchagua na nyumba ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako, nakusihi usikie sala yao na maombi yao ukiwa huko mbinguni na uwapatie ushindi vitani. “Ikiwa watatenda dhambi dhidi yako, maana hakuna mtu asiyetenda dhambi, na ukiwakasirikia na kuwaacha washindwe na adui, hata wapelekwe mateka mpaka nchi ya mbali au ya karibu; kama watakapokuwa huko uhamishoni watajirudi kwa roho yao yote na kwa moyo wao wote na kutubu na kukuomba msamaha, wakisema, ‘Tumetenda dhambi; tumepotoka na kufanya maovu’; pia kama watatubu kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote wakati watakapokuwa katika nchi ya uhamisho, na kama watakuomba wakielekea nchi yao ambayo uliwapatia babu zao, mji huu ambao uliuchagua na nyumba hii ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako; basi, nakusihi usikie huko mbinguni uliko sala yao na maombi yao na uwapatie haki zao, uwasamehe watu wako ambao wametenda dhambi dhidi yako. “Sasa ee Mungu wangu, tuangalie na upokee maombi tutakayoomba mahali hapa. Sasa inuka ee Bwana Mungu, uingie mahali pako pa kupumzika wewe pamoja na sanduku la agano la nguvu zako. Makuhani wako ee Bwana Mungu, wapate wokovu, na watakatifu wako wafurahie wema wako. Ee Bwana Mungu, usimpige kisogo masiha wako. Kumbuka fadhili zako kwa mtumishi wako Daudi.” Solomoni alipomaliza sala yake, moto ulishuka kutoka mbinguni na kuchoma sadaka na tambiko za kuteketeza zilizotolewa, kisha utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukaijaza nyumba. Kwa kuwa utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulijaa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, makuhani hawakuweza kuingia humo. Waisraeli wote walipoona moto ukishuka kutoka mbinguni na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulijaa katika nyumba walisujudu nyuso zao zikifika mpaka sakafuni, wakamwabudu na kumshukuru Mwenyezi-Mungu wakisema, “Kwa kuwa ni mwema, fadhili zake zadumu milele.” Kisha mfalme Solomoni na watu wote walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko. Naye Solomoni alimtolea Bwana ng'ombe 22,000 na kondoo 120,000. Hivyo ndivyo Solomoni na watu wote walivyoiweka wakfu nyumba ya Mungu. Makuhani walisimama mahali maalumu walipoagizwa kusimama, nao Walawi walisimama wakiwa na vyombo vya Mwenyezi-Mungu vya muziki mfalme Daudi alivyovitengeneza kwa ajili ya kutoa shukrani kwa Mwenyezi-Mungu. Waliimba, “Kwa kuwa fadhili zake zadumu milele,” Daudi alivyowaagiza. Makuhani walipiga tarumbeta hali Waisraeli wote walikuwa wamesimama. Basi, mfalme Solomoni akaiweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kwani hapo ndipo alipotolea sadaka za kuteketezwa na mafuta ya sadaka za amani, kwa sababu ile madhabahu ya shaba haikutosha kwa sadaka hizo zote. Naye Solomoni kwa muda wa siku saba alifanya sikukuu pamoja na kusanyiko kubwa la watu wote wa Israeli waliotoka kiingilio cha Hamathi mpaka mto wa Misri. Siku ya nane, walikusanyika wakafanya ibada maalumu baada ya muda wa siku saba walizotumia kuitakasa meza ya matoleo ya sadaka, na siku saba nyingine za sikukuu. Siku iliyofuata ambayo ilikuwa siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa saba, Solomoni aliwaaga watu waende kwao, wakishangilia na kufurahi moyoni kwa sababu ya wema ambao Mwenyezi-Mungu aliowajalia Daudi, Solomoni na watu wake Israeli. Basi, mfalme Solomoni alimaliza kuijenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu na alifaulu kuyatekeleza yale yote aliyokusudia kuifanyia nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu. Kisha Mwenyezi-Mungu alimtokea usiku, akamwambia, “Nimesikia sala yako na nimepachagua mahali hapa pawe nyumba yangu ya kunitolea tambiko. Nikiwanyima mvua ama nikiwaletea nzige wale mimea yao au wakipatwa na maradhi mabaya kama watu hao wangu wakijinyenyekesha, wakasali, wakanitafuta na kuacha njia zao mbaya, basi, mimi nitawasikiliza kutoka juu mbinguni; nitawasamehe dhambi yao na kuistawisha nchi yao. Sasa nitalichunga hekalu hili na kusikiliza maombi yatakayofanyika hapa, kwa maana nimeitakasa nyumba hii ili watu waliabudu jina langu hapa milele. Nitailinda na kuipenda daima. Nawe, kama ukinitumikia kwa uaminifu kama Daudi baba yako alivyofanya, ukitenda yote niliyokuamuru na kutii maongozi yangu na maagizo yangu, basi, mimi nitakiimarisha kiti chako cha ufalme kama nilivyofanya agano na Daudi baba yako nikisema, ‘Hutakosa mtu wa kutawala Israeli.’ Lakini mkiacha kunifuata, mkayaasi maongozi yangu na amri nilizowapa, na kwenda kutumikia miungu mingine na kuiabudu, kwa sababu hiyo mimi nitawangoeni kutoka nchi hii ambayo nimewapa. Kadhalika na nyumba hii ambayo nimeiweka wakfu kwa ajili ya jina langu nitaitupilia mbali nami, na kuifanya kitu cha kupuuzwa na kudharauliwa miongoni mwa mataifa yote. Na juu ya nyumba hii ambayo nimetukuka, kila apitaye karibu atashtuka na kuuliza, ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu amefanya hivyo kwa nchi hii na kwa nyumba hii?’ Watu wengine watajibu, ‘Ni kwa sababu walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao aliyewatoa nchini Misri; wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia. Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu amewaletea maafa haya yote.’” Miaka ishirini, ambayo Solomoni aliijenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu ilipokwisha kupita, Solomoni aliijenga upya miji aliyopewa na Huramu, halafu akawapa Waisraeli miji hiyo waishi humo. Baadaye Solomoni alielekea Hamath-zoba na kuuteka, na kuujenga mji wa Tadmori nyikani. Aliijenga upya miji ya ghala iliyokuwa huko Hamathi. Kadhalika, Solomoni alijenga miji ifuatayo: Beth-horoni wa juu, na Beth-horoni wa chini, miji yenye ngome, kuta, malango na makomeo, mji wa Baalathi, na miji yake yote ya ghala, magari yake ya kukokotwa na ya wapandafarasi wake, na chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, Lebanoni au kwingineko katika ufalme wake. Watu wengine wote waliobaki miongoni mwa Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, yaani wote ambao hawakuwa Waisraeli, pia wazawa wao ambao Waisraeli hawakuwaangamiza, Solomoni aliwafanyiza kazi za kulazimishwa, na hivi ndivyo wanavyofanya hata sasa. Lakini kati ya watu wa Israeli, Solomoni hakumfanya mtu yeyote kuwa mtumwa kwa ajili ya kazi yake; wao walikuwa askari, makamanda wa maofisa wake, makamanda wa magari yake ya kukokotwa na wapandafarasi wake. Ifuatayo ndiyo jumla ya maofisa wakuu wa mfalme Solomoni: Walikuwa 250, waliokuwa na mamlaka juu ya watu. Solomoni alimhamisha binti Farao mfalme wa Misri, kutoka mji wa Daudi, akampeleka kwenye nyumba aliyomjengea. Alisema, “Mke wangu hataishi katika nyumba ya Daudi mfalme wa Israeli, kwa maana mahali pote ambapo sanduku la Mwenyezi-Mungu limekuwa, ni patakatifu.” Solomoni alimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za kuteketeza juu ya madhabahu aliyokuwa amemjengea Mwenyezi-Mungu mbele ya ukumbi wa hekalu. Alitoa tambiko hizo kadiri ilivyotakiwa na amri ya Mose kila siku takatifu, yaani siku za Sabato, sikukuu za mwezi mwandamo, na sikukuu tatu za kila mwaka — sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, sikukuu ya majuma na sikukuu ya vibanda. Akifuata maagizo ya Daudi baba yake, alipanga zamu za kila siku za makuhani na za Walawi waliowasaidia makuhani kusifu na kuzitekeleza kazi zao. Kadhalika aliwapanga walinda malango katika makundi aliyoyaweka kulinda kila lango; maana ndivyo alivyoamuru Daudi, mtu wa Mungu. Nao hawakuyaacha maagizo mfalme aliyowaamuru makuhani na Walawi jambo lolote na kuhusu hazina. Basi miradi yote ya Solomoni aliyofanya tangu jiwe la msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu lilipowekwa ilikamilika. Hivyo nyumba ya Mwenyezi-Mungu ilimalizika. Kisha Solomoni alikwenda Esion-geberi na Elothi iliyo pwani mwa bahari, katika nchi ya Edomu. Huramu alimpelekea merikebu zilizokuwa chini ya uongozi wa maofisa wake, pamoja na mabaharia stadi. Hao, pamoja na maofisa wa Solomoni, walisafiri hadi Ofiri, na kuchukua kutoka huko dhahabu, wakamletea mfalme Solomoni kiasi cha kilo 15,000. Malkia wa Sheba aliposikia sifa za Solomoni, aliwasili Yerusalemu ili kumjaribu Solomoni kwa maswali magumu. Alifuatana na msafara wa watu, pamoja na ngamia waliobeba manukato, dhahabu nyingi sana na vito vya thamani. Na alipofika kwa Solomoni, alimwuliza maswali yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. Solomoni aliyajibu maswali yote; hapakuwapo na jambo lolote aliloshindwa kumweleza. Malkia wa Sheba alipoiona hekima ya Solomoni na nyumba aliyokuwa ameijenga, tena alipotazama chakula kilichoandaliwa mezani pwake na kuona jinsi maofisa wake walivyoketi mezani na huduma ya watumishi wake na jinsi walivyovalia; pia wanyweshaji wake na jinsi walivyovalia, tambiko za kuteketeza ambazo alizitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alipoona hayo yote akashangaa sana. Basi, akamwambia mfalme, “Yote niliyosikia nchini kwangu kuhusu kazi zako na hekima yako ni ya kweli! Lakini sikuweza kuamini habari zao mpaka nilipofika na kujionea mwenyewe, na kumbe niliambiwa nusu tu; hekima yako na ufanisi wako ni zaidi ya yale niliyosikia. Wana bahati wake zako! Wana bahati hawa watumishi wako ambao daima husimama mbele yako na kusikiliza hekima yako! Na asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ambaye amependezwa nawe, akakuketisha juu ya kiti chake cha enzi, uwe mfalme kwa niaba yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Kwa sababu Mungu wako amewapenda Waisraeli na kuwaimarisha milele, amekuweka wewe uwe mfalme juu yao ili udumishe haki na uadilifu.” Kisha akampa mfalme zaidi ya kilo 4,000 za dhahabu, na kiasi kikubwa cha manukato na vito vya thamani. Aina ya manukato ambayo huyo malkia wa Sheba alimpatia mfalme Solomoni, ilikuwa ya pekee. Kadhalika, watumishi wa Huramu pamoja na watumishi wa Solomoni walioleta dhahabu kutoka Ofiri, walileta pia miti ya misandali na mawe ya thamani. Solomoni alitumia miti hiyo kutengeneza madari ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu, na pia kutengenezea vinubi na vinanda vya waimbaji. Mambo ya namna hiyo hayakuwa yameonekana kamwe katika nchi ya Yuda. Naye mfalme Solomoni alimpatia malkia wa Sheba kila kitu alichotamani, chochote alichoomba mbali na vitu alivyomletea mfalme. Hatimaye malkia aliondoka akarudi katika nchi yake akiwa pamoja na watumishi wake. Kila mwaka, Solomoni alipelekewa dhahabu kadiri ya kilo 23,000, mbali na dhahabu aliyopokea kutoka kwa wafanyabiashara na wachuuzi. Wafalme wote wa Arabia na wakuu wa mikoa ya Israeli pia walimletea Solomoni fedha na dhahabu. Mfalme Solomoni alitengeneza ngao kubwa 200; kila moja ilipakwa kadiri ya kilo saba za dhahabu iliyofuliwa. Pia alitengeneza ngao ndogondogo 300, kila moja ilipakwa dhahabu ipatayo kilo tatu, halafu mfalme akaziweka katika jengo lililoitwa Nyumba ya Msitu wa Lebanoni. Hali kadhalika mfalme alitengeneza kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza dhahabu safi. Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na kiti cha kuegemea miguu cha dhahabu, vyote hivyo vilikuwa vimeshikamanishwa na kiti hicho cha enzi; na kila upande kilikuwa na mahali pa kuegemeza mikono; pia kilikuwa na sanamu mbili za simba karibu na mahali hapo pa kuegemeza mikono. Palikuwa na sanamu kumi na mbili za simba waliosimama mwishoni mwa kila ngazi. Kiti kama hicho kilikuwa hakijawahi kutengenezwa katika ufalme wowote ule. Vikombe vyote vya mfalme Solomoni vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vilivyokuwa katika Nyumba ya Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Fedha haikuhesabiwa kuwa kitu cha thamani katika siku za Solomoni. Solomoni alikuwa na merikebu zilizosafiri mpaka Tarshishi na watumishi wa Huramu, na kila baada ya miaka mitatu, merikebu hizo zilirudi zikimletea dhahabu, fedha, pembe, nyani na tausi. Mfalme Solomoni aliwapita wafalme wote duniani kwa mali na kwa hekima. Nao wafalme wa nchi zote walikuwa na hamu ya kumwendea Solomoni ili kusikiliza hekima yake ambayo Mungu alikuwa amemjalia. Kila mmoja wao alimletea zawadi: Vyombo vya fedha na vya dhahabu, mavazi na silaha manukato, farasi na nyumbu. Zawadi hizi alizipokea kila mwaka. Mfalme Solomoni akawa na vibanda 4,000 vya kuwekea farasi na magari, na askari wapandafarasi 12,000 ambao aliwaweka katika miji yenye vituo vya magari ya farasi na katika Yerusalemu. Aliwatawala wafalme wote waliokuwako kuanzia mto Eufrate, hadi nchi ya Wafilisti na hadi mpakani na Misri. Basi Solomoni alifanya fedha katika Yerusalemu kuwa kitu cha kawaida kama mawe katika Yerusalemu, na mbao za mierezi zilipatikana kwa wingi kama mikuyu iliyomo Shefela. Solomoni aliletewa farasi walionunuliwa kutoka Misri na nchi nyinginezo. Matendo mengine ya Solomoni, kutoka mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha “Historia ya Nabii Nathani,” katika “Unabii wa Ahiya wa Shilo,” na katika “Maono ya Ido” mwonaji, ambayo yahusu pia Yeroboamu mwana wa Nebati. Solomoni alitawala nchi yote ya Israeli kwa miaka arubaini. Hatimaye Solomoni alifariki dunia na kuzikwa katika mji wa Daudi baba yake. Rehoboamu, mwanawe, akatawala mahali pake. Basi, Rehoboamu akaenda Shekemu, ambako Waisraeli wote walikuwa wamekusanyika ili kumtawaza awe mfalme. Naye Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari kuhusu tendo hilo (wakati huo alikuwa bado anaishi Misri alikokwenda alipomkimbia Solomoni) alitoka Misri. Lakini Waisraeli walituma ujumbe na kumwita. Kisha, yeye pamoja na Waisraeli wote walimwendea Rehoboamu na kumwambia, “Baba yako alitutwika mzigo mzito. Basi, utupunguzie mzigo huo, nasi tutakutumikia.” Rehoboamu akawajibu, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.” Basi wakaondoka. Baadaye, Rehoboamu alitaka kujua maoni ya wazee ambao walikuwa washauri wa Solomoni, baba yake, alipokuwa angali hai, akawauliza, “Je, mnanishauri niwape jibu gani watu hawa?” Wazee hao wakamjibu, “Ukiwahurumia watu hawa, ukiwafurahisha na kusema nao maneno mazuri, hapo watakuwa watumishi wako daima.” Lakini Rehoboamu alipuuza shauri la wazee na badala yake akashauriana na vijana wa rika lake ambao walikuwa washauri wake. Basi, akawauliza, “Nyinyi mnatoa shauri gani ili tuweze kuwajibu watu hawa walioniambia, ‘Punguza mzigo ambao baba yako alitutwika?’” Hao vijana wakamjibu, “Watu hao waliokuambia ‘Baba yako alitutwika mzigo mzito, lakini wewe utupunguzie,’ wewe waambie hivi: ‘Kidole changu kidogo cha mwisho ni kinene zaidi kuliko kiuno cha baba yangu. Mzigo wa baba yangu ulikuwa mzito, lakini wangu utakuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.’” Basi katika siku ya tatu Yeroboamu pamoja na watu wote wakarudi kwa Rehoboamu kama alivyokuwa amewaagiza. Naye mfalme Rehoboamu akawajibu kwa ukali, akapuuza shauri la wazee, na kufuata shauri la vijana wenzake. Basi akasema, “Baba yangu aliwatwika mzigo mzito, lakini mimi nitaufanya kuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba” Hivyo mfalme hakuwajali watu kwa sababu jambo hili lilisababishwa na Mungu ili Mwenyezi-Mungu atimize neno lake alilomwambia Yeroboamu, mwana wa Nebati kwa njia ya Ahiya wa Shilo. Lakini watu wote wa Israeli walipoona kwamba mfalme hakuwajali walimwambia, “Tuna sehemu gani kwa Daudi? Hatuna urithi katika mwana wa Yese. Kila mmoja na arudi nyumbani kwake, enyi watu wa Israeli. Itunze nyumba yako mwenyewe, ee Daudi.” Hivyo watu wote wa Israeli wakarudi makwao. Lakini Rehoboamu alitawala watu wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda. Kisha mfalme Rehoboamu alipomtuma Hadoramu aliyekuwa mnyapara mkuu wa kazi za kulazimishwa, watu wa Israeli walimpiga mawe, wakamuua. Ndipo Rehoboamu alipopanda gari lake haraka akakimbilia Yerusalemu. Hivyo, watu wa Israeli wamekuwa katika hali ya maasi dhidi ya utawala wa ukoo wa Daudi mpaka leo. Rehoboamu alipofika Yerusalemu, alikusanya askari stadi180,000 wa makabila ya Yuda na Benyamini, apate kupigana na Israeli, ili ajirudishie huo ufalme. Lakini ujumbe wa Mungu ulimjia Shemaya mtu wa Mungu, kusema: “Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni, mfalme wa Yuda na Waisraeli wote katika Yuda na Benyamini ya kwamba mimi Bwana nasema, ‘Msiende wala msipigane na ndugu zenu. Rudini kila mtu nyumbani kwake, maana hayo yaliyotokea ni kama nilivyopanga.’” Basi wakatii ujumbe wa Mwenyezi-Mungu, wakarudi nyumbani, wala hawakwenda kupigana na Yeroboamu. Rehoboamu alikaa Yerusalemu na akajenga ngome na kuiimarisha miji ifuatayo iliyokuwa nchini Yuda: Bethlehemu, Etamu, Tekoa, Beth-suri, Soko, Adulamu, Gathi, Maresha, Zifu, Adoraimu, Lakishi, Azeka, Sora, Ayaloni na Hebroni. Miji hiyo yenye ngome imo Yuda na Benyamini. Aliziimarisha ngome hizo na humo ndani akaweka makamanda na maghala ya vyakula, mafuta na divai. Ndani ya kila mji, aliweka ngao na mikuki, na kuifanya miji hiyo kuwa imara sana. Yuda na Benyamini zikawa chini ya mamlaka yake. Makuhani na Walawi wote waliokuwa wanaishi kote nchini Israeli, walimwendea kutoka maeneo yao. Walawi waliyaacha malisho yao, na maeneo yao mengine kwa sababu Yeroboamu na wanawe waliwakataza kumtumikia Mwenyezi-Mungu kama makuhani wa Mwenyezi-Mungu. Yeroboamu alijichagulia makuhani wake mwenyewe wa kuhudumu mahali pa juu pa kuabudia miungu na yale majini na sanamu za ndama alizojitengenezea. Watu wote ambao walikuwa wamenuia kwa moyo wa dhati kumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kutoka katika makabila yote ya Israeli, waliandamana na Walawi hadi Yerusalemu ili wapate kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. Hivyo, waliuimarisha ufalme wa Yuda, na kwa muda wa miaka mitatu, wakauunga mkono utawala wa Rehoboamu mwanawe Solomoni, nao ukawa imara na wakaishi katika hali ileile waliyoishi wakati walipokuwa chini ya utawala wa mfalme Daudi na mfalme Solomoni. Rehoboamu alioa mke, jina lake Mahalathi binti Yeremothi mwana wa Daudi. Mama yake alikuwa Abihaili binti Eliabu, mwana wa Yese. Naye alimzalia wana watatu: Yeushi, Shemaria na Zahamu. Baadaye, alimwoa Maaka binti Absalomu, naye akamzalia Abiya, Atai, Ziza na Shelomithi. Rehoboamu alioa wake kumi na wanane na masuria sitini, akazaa watoto wa kiume ishirini na wanne na mabinti sitini. Miongoni mwa wake zake wote na masuria wake, alimpenda Maaka binti Absalomu zaidi. Hivyo akamchagua Abiya, mwana wa Maaka, awe mkuu kati ya ndugu zake, kwani alinuia kumfanya awe mfalme. Rehoboamu alifanya jambo la busara, akawatawanya baadhi ya wanawe katika nchi yote ya Yuda na Benyamini akiwaweka katika miji yote yenye ngome. Wakiwa humo, aliwapa vyakula tele na pia akawaoza wake wengi. Ikawa utawala wa Rehoboamu ulipokwisha imarika na kuwa na nguvu, yeye pamoja na watu wake wote waliacha kutii sheria ya Mwenyezi-Mungu. Katika mwaka wa tano wa utawala wake, kwa sababu hawakumtii Mwenyezi-Mungu, Shishaki, mfalme wa Misri aliushambulia Yerusalemu, akiwa na magari 1,200, wapandafarasi 60,000, na askari wengi mno wasiohesabika, waliotoka Misri pamoja naye: Walibia, Wasukii na Waethiopia. Aliiteka miji yenye ngome katika Yuda, akafika hadi Yerusalemu. Kisha Nabii Shemaya alimwendea mfalme Rehoboamu na wakuu wa Yuda, waliokusanyika Yerusalemu ambapo walikimbilia ili kumwepuka Shishaki, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Nyinyi mmeniacha mimi, kwa hiyo basi, nami nimewaacha nyinyi na kuwatia mikononi mwa Shishaki.’” Ndipo wakuu wa Israeli na mfalme wakajinyenyekesha, wakasema, “Mwenyezi-Mungu ametenda sawa.” Mwenyezi-Mungu alipoona ya kuwa wamejinyenyekesha, alizungumza tena na nabii Shemaya, akamwambia, “Wamejinyenyekesha, sitawaangamiza, bali nitawaokoa baada ya muda mfupi. Sitaushushia mji wa Yerusalemu ghadhabu yangu kuuharibu kwa mkono wa Shishaki, lakini watamtumikia ili wapate kujua tofauti iliyopo kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa duniani.” Basi, mfalme Shishaki wa Misri aliushambulia Yerusalemu, akaichukua hazina yote ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya ikulu, pamoja na ngao za dhahabu alizozitengeneza mfalme Solomoni. Badala ya ngao hizo, mfalme Rehoboamu alitengeneza ngao za shaba na kuziweka chini ya ulinzi wa wangojamlango wa ikulu. Kila wakati mfalme alipokwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walinzi waliiingia wakazibeba ngao hizo na baadaye wakazirudisha katika chumba cha ulinzi. Alipojinyenyekesha, Mwenyezi-Mungu aliacha kumghadhibikia na hakumwangamiza kabisa. Zaidi ya hayo, hali ya nchi ya Yuda ilikuwa nzuri. Hivyo mfalme Rehoboamu alijiimarisha zaidi katika Yerusalemu, akaitawala Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arubaini na mmoja alipoanza kutawala Yuda. Naye alitawala kwa muda wa miaka kumi na saba katika Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi-Mungu aliuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli aabudiwe humo. Mama yake Rehoboamu aliitwa Naama, kutoka Amoni. Rehoboamu alitenda maovu, kwa maana hakunuia kumtafuta Mwenyezi-Mungu kwa moyo. Matendo yote ya mfalme Rehoboamu ya mwanzo mpaka ya mwisho na rekodi ya ukoo yameandikwa katika kitabu cha Kumbukumbu za nabii Shemaya, na Kumbukumbu za Ido Mwonaji. Wakati huu wote, kulikuwa na vita vya mfululizo kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. Hatimaye Rehoboamu alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi, na Abiya mwanawe, akatawala mahali pake. Abiya alianza kutawala Yuda mnamo mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yeroboamu. Alitawala kwa muda wa miaka mitatu akiwa Yerusalemu. Mama yake alikuwa Maaka binti Urieli wa Gibea. Kulitokea vita kati ya Abiya na Yeroboamu. Abiya alijiandaa kupigana vita akiwa na jeshi la askari hodari 400,000, naye Yeroboamu akamkabili na jeshi lake la askari hodari 800,000. Mfalme Abiya alisimama juu ya mlima Semaraimu, ulioko kati ya milima ya Efraimu, akamwambia Yeroboamu na watu wa Israeli, “Nisikilize ewe Yeroboamu na watu wote wa Israeli! Je, hamjui kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alimwahidi Daudi kwa kufanya naye agano lisilovunjika kuwa daima, wafalme wote wa Israeli watatoka katika uzao wake? Lakini Yeroboamu mwana wa Nebati mtumishi wa Solomoni, mwana wa Daudi alimwasi bwana wake. Baadaye, alijikusanyia kikundi cha mabaradhuli, watu wapumbavu wasiofaa kitu, nao wakamshawishi Rehoboamu mwana wa Solomoni, kutenda yale waliyotaka wao, naye hangeweza kuwazuia kwani wakati huo alikuwa bado kijana bila uzoefu mwingi. “Sasa nyinyi mnadhani mnaweza kupinga ufalme wa Mwenyezi-Mungu aliopewa Daudi na uzao wake kwa sababu eti mnalo jeshi kubwa na sanamu za dhahabu za ndama, alizowatengenezea Yeroboamu kuwa miungu yenu! Je, hamkuwafukuza makuhani wa Mwenyezi-Mungu, wana wa Aroni, kadhalika na Walawi, na kujifanyia makuhani wenu wenyewe kama wafanyavyo watu wa mataifa mengine? Yeyote ajaye kwenu kujiweka wakfu na ndama dume ama kondoo madume saba, huwa kuhani wa vitu ambavyo si miungu. “Lakini kuhusu sisi, Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu, wala hatujamwacha. Tena tunao makuhani wa uzao wa Aroni ambao wanamtumikia Mwenyezi-Mungu, nao husaidiwa na Walawi. Kila siku asubuhi na jioni, makuhani humtolea sadaka za kuteketezwa nzima, na kumfukizia ubani wenye harufu nzuri, tena hupanga juu ya meza ya dhahabu safi, mikate ya kuwekwa mbele ya Mungu, na kukitunza kinara cha dhahabu na kuziwasha taa kila siku jioni. Sisi tunayafuata maagizo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, lakini nyinyi mmemwacha. Hebu tazameni, Mungu mwenyewe ndiye kiongozi wetu na makuhani wake wanazo tarumbeta zao tayari kuzipiga ili kutupa ishara ya kuanza vita dhidi yenu. Enyi watu wa Israeli, acheni kupigana vita dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu. Hamwezi kushinda!” Lakini wakati huo, Yeroboamu alikuwa amekwisha tuma baadhi ya wanajeshi wake kulivamia jeshi la Yuda kutoka upande wa nyuma, hali wale wengine wamewakabili kutoka upande wa mbele. Watu wa Yuda walipotazama nyuma, walishtuka kuona wamezingirwa; basi walimlilia Mwenyezi-Mungu, nao makuhani wakazipiga tarumbeta zao. Ndipo wanajeshi wa Yuda wakapiga kelele ya vita, na walipofanya hivyo, Mungu alimshinda Yeroboamu na jeshi lake la watu wa Israeli mbele ya Abiya na watu wa Yuda. Watu wa Israeli waliwakimbia watu wa Yuda naye Mungu akawatia mikononi mwao. Abiya na jeshi lake aliwashambulia sana, akawashinda; akaua wanajeshi wa Israeli, laki tano waliokuwa baadhi ya wanajeshi hodari sana katika Israeli. Kwa hiyo, watu wa Yuda walipata ushindi dhidi ya watu wa Israeli kwa sababu walimtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. Abiya alimfukuza Yeroboamu, akamnyanganya baadhi ya miji yake: Betheli, Yeshana, Efroni pamoja na vijiji vilivyokuwa kandokando ya miji hiyo. Yeroboamu hakuweza kupata nguvu tena wakati wa Abiya. Mwishowe Mwenyezi-Mungu alimpiga, naye akafa. Lakini Abiya aliendelea kupata nguvu zaidi. Akaoa wanawake kumi na wanne, akapata watoto wa kiume ishirini na wawili na mabinti kumi na sita. Matendo mengine ya Abiya, shughuli zake na maneno yake, yameandikwa katika kitabu cha “Historia ya Nabii Ido.” Mwishowe, Abiya alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi na Asa mwanawe akatawala mahali pake. Wakati wa Asa, kulikuwa na amani nchini kwa muda wa miaka kumi. Asa alitenda yaliyokuwa mazuri na mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. Aliondoa nchini madhabahu za kigeni na mahali pa kuabudia miungu mingine, akabomoa minara na kuzikatakata sanamu za Ashera. Aliwaamuru watu wa Yuda wamtafute Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, na kuzitii sheria na amri. Pia aliondoa mahali pote pa kuabudia miungu mingine na meza za kufukizia ubani kutoka katika miji yote ya Yuda; halafu ufalme wake ulikuwa na amani chini ya utawala wake. Alijenga miji yenye ngome katika Yuda wakati huo wa amani, na kwa muda wa miaka kadhaa, hapakutokea vita kwa maana Mwenyezi-Mungu alimpa amani. Naye akawaambia watu wa Yuda, “Na tuiimarishe miji kwa kuizungushia kuta na minara na malango yenye makomeo. Nchi bado imo mikononi mwetu kwa maana tumeyatenda mapenzi yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, naye ametupa amani pande zote.” Basi wakajenga, wakafanikiwa. Mfalme Asa alikuwa na jeshi la askari 300,000 kutoka Yuda, wenye ngao na mikuki, na wengine 280,000 kutoka Benyamini, wenye ngao na pinde. Wote walikuwa watu mashujaa sana. Zera, Mwethiopia aliishambulia nchi ya Yuda akiwa na jeshi la askari 1,000,000 na magari 300, akasonga mbele hadi Maresha. Asa alitoka akaenda kupigana naye. Pande zote mbili zilijipanga katika bonde la Sefatha karibu na Maresha. Hapo Asa akamlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, hakuna mwingine kama wewe, mwenye uwezo wa kulisaidia jeshi liwe dhaifu au lenye nguvu. Tusaidie, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa kuwa sisi tunakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja kupigana na jeshi hili kubwa ajabu. Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe Mungu wetu; usimruhusu binadamu yeyote ashindane nawe.” Basi, Mwenyezi-Mungu aliwashinda Waethiopia mbele ya Asa na jeshi lake la watu wa Yuda. Waethiopia wakakimbia. Asa pamoja na wanajeshi wake wakawafuatilia mpaka Gerari, wakawaua Waethiopia wengi sana, asibaki hata mmoja, kwani walikuwa wamekwisha shindwa na Mwenyezi-Mungu pamoja na jeshi lake. Jeshi la Yuda lilichukua nyara nyingi sana. Liliharibu miji yote iliyokuwa kandokando ya Gerari, kwa kuwa watu waliokuwamo katika miji hiyo waliingiwa na hofu ya Mwenyezi-Mungu. Jeshi lilichukua mali nyingi kutoka katika miji hiyo kwa sababu kulikuwamo mali nyingi sana. Lilishambulia pia wachungaji, likachukua kondoo wengi na ngamia. Kisha likarejea Yerusalemu. Roho ya Mungu ilimjia Azaria mwana wa Odedi, naye akatoka kwenda kumlaki mfalme Asa, akamwambia, “Nisikilize, ee mfalme Asa na watu wote wa Yuda na Benyamini! Mwenyezi-Mungu yu pamoja nanyi, ikiwa mtakuwa pamoja naye. Mkimtafuta, mtampata, lakini mkimwacha naye atawaacha. Kwa muda mrefu sasa, Waisraeli wameishi bila Mungu wa kweli, wala makuhani wa kuwafundisha, na bila sheria. Lakini walipopatwa na shida, walimgeukia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, wakamtafuta, wakampata. Zamani hizo, hakuna mtu aliyeweza kuingia wala kutoka kwa usalama kwa sababu hapakuwa na amani; ghasia nyingi mno ziliwasumbua wananchi wa kila nchi. Kulijaa mafarakano mengi, taifa moja lilipigana na taifa lingine na mji mmoja ulipigana na mji mwingine, kwa sababu Mungu aliwafadhaisha kwa taabu za kila aina. Lakini nyinyi jipeni moyo, wala msilegee kwa maana mtapata tuzo kwa kazi mfanyayo.” Asa alipoyasikia maneno haya, yaani unabii wa Azaria mwana wa Odedi, alipata moyo. Akaziondoa sanamu zote za kuchukiza katika nchi yote ya Yuda na Benyamini, na kutoka katika miji yote aliyoiteka katika nchi ya milima ya Efraimu. Pia, akaitengeneza upya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu iliyokuwa katika ukumbi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Asa aliwaita watu wote wa Yuda na Benyamini, na wengine wote waliokuwa wakikaa nchini mwake kutoka Efraimu, Manase na Simeoni. Hawa walikuja kwake walipoona kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, alikuwa pamoja naye. Wote walikusanyika Yerusalemu katika mwezi wa tatu wa mwaka wa kumi na tano wa utawala wake Asa. Siku hiyo, walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za ng'ombe 700 na kondoo 7,000, kutoka katika zile nyara walizoteka. Hapo wakafanya agano, ya kuwa watamtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, kwa moyo wote na kwa roho yao yote; na kwamba yeyote asiyemtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, awe kijana au mzee, mwanamume au mwanamke, sharti auawe. Walimwapia Mwenyezi-Mungu kwa sauti kuu, wakapaza sauti zaidi, wakapiga tarumbeta na baragumu. Watu wote wa Yuda walikuwa na furaha tele kwa kuwa walikuwa wameapa kwa moyo wote. Walikuwa wamemtafuta kwa dhati, wakampata. Naye Mwenyezi-Mungu akawapa amani pande zote. Mfalme Asa alimwondoa hata Maaka, mama yake, katika cheo chake cha mama malkia, kwa sababu alitengeneza sanamu ya kuchukiza ya Ashera, mungu wa kike. Asa alikatilia mbali sanamu hiyo, akaipondaponda na kuiteketeza katika bonde la kijito Kidroni. Lakini hata hivyo mahali pa kutambikia miungu mingine katika Israeli hapakuharibiwa; lakini yeye alikuwa na moyo mwaminifu maisha yake yote. Alivirudisha katika nyumba ya Mungu vifaa vyote vilivyowekwa wakfu na baba yake pamoja na vile alivyoviweka wakfu yeye mwenyewe: Fedha na dhahabu na vyombo vinginevyo. Hapakuwa na vita tena nchini mpaka mwaka wa thelathini na tano wa utawala wake Asa. Katika mwaka wa thelathini na sita wa utawala wa mfalme Asa, Baasha, mfalme wa Israeli, aliishambulia nchi ya Yuda na kuanza kuujenga mji wa Rama ili apate kuzuia mtu yeyote asitoke wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda. Ndipo mfalme Asa akachukua fedha na dhahabu kutoka katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu, akazituma Damasko kwa Ben-hadadi, mfalme wa Aramu na ujumbe akasema, “Na tufanye mkataba wa ushirikiano kati yangu na wewe kama walivyofanya baba yangu na baba yako; tazama nakupa zawadi ya fedha na dhahabu; nenda ukavunje mkataba wa ushirikiano ulioko kati yako na mfalme Baasha wa Israeli ili aache mashambulizi dhidi yangu.” Hapo mfalme Ben-hadadi alikubali pendekezo la mfalme Asa, akawatuma majemadari wake na majeshi yake kwenda kuishambulia miji ya Israeli. Nao waliiteka miji ya Iyoni, Dani, Abel-maimu, na miji yote ya Naftali iliyokuwa na ghala za vyakula. Mfalme Baasha alipopata habari za mashambulizi hayo, aliacha kuujenga mji wa Rama, akasimamisha kazi yake. Ndipo mfalme Asa alipowapeleka watu wote wa Yuda, wakahamisha mawe ya Rama na mbao, vifaa ambavyo Baasha alivitumia kujengea. Kisha Asa alitumia vifaa hivyo kujengea miji ya Geba na Mizpa. Wakati huo, Hanani mwonaji alimwendea mfalme Asa wa Yuda, akamwambia, “Kwa sababu ulimtegemea mfalme wa Shamu badala ya kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, jeshi la mfalme wa Shamu limekuponyoka. Je, wale Waethiopia na Walibia hawakuwa jeshi kubwa na magari na wapandafarasi wengi? Lakini kwa vile ulimtegemea Mwenyezi-Mungu, yeye aliwatia mikononi mwako. Mwenyezi-Mungu huuchunga kwa makini ulimwengu wote, ili kuwapa nguvu wale walio waaminifu kwake. Umetenda jambo la kipumbavu, kwa hiyo tangu sasa, utakuwa na vita kila mara.” Maneno haya yalimfanya Asa amkasirikie sana Hanani mwonaji, hata akamfunga gerezani. Wakati huohuo, Asa alianza kuwatesa vikali baadhi ya watu. Matendo ya Asa, toka mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha “Wafalme wa Yuda na Israeli.” Katika mwaka wa thelathini na tisa wa ufalme wake, Asa alishikwa na ugonjwa wa miguu, akaugua sana. Lakini hata wakati huo, Asa hakumgeukia Mwenyezi-Mungu amsaidie, bali alijitafutia msaada kutoka kwa waganga. Hatimaye Asa alifariki mnamo mwaka wa arubaini na moja wa utawala wake. Alizikwa katika kaburi alilokuwa amejichimbia mwenyewe mwambani, katika mji wa Daudi. Walimlaza ndani ya jeneza lililokuwa limejazwa manukato ya kila aina yaliyotayarishwa na mafundi wa kutengeneza marashi, wakawasha moto mkubwa sana kwa heshima yake. Naye Yehoshafati mwanawe alitawala mahali pa baba yake Asa, akajiimarisha dhidi ya Israeli. Aliweka majeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome, na katika maeneo mengine ya Yuda, na katika miji ya Efraimu ambayo Asa baba yake aliiteka akaweka askari walinzi. Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yehoshafati kwa sababu alifuata njia za awali za baba yake, na wala hakumwabudu Baali. Yeye alimtafuta Mungu wa baba yake na kuzitii amri zake, wala hakufuata matendo ya watu wa Israeli. Mwenyezi-Mungu, aliuimarisha ufalme wa Yuda mikononi mwa Yehoshafati, nao watu wote wakamletea zawadi, akatajirika sana na kuheshimika. Alipenda sana moyoni kumtumikia Mwenyezi-Mungu, na zaidi ya hayo, alipaharibu mahali pote pa kuabudia miungu mingine na sanamu za Ashera, mungu wa kike, nchini Yuda. Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wake, Yehoshafati aliwatuma maofisa wafuatao wakafundishe katika miji ya Yuda: Ben-haili, Obadia, Zekaria, Nethaneli na Mikaya. Walawi tisa na Makuhani wawili waliandamana nao. Walawi hao walikuwa Shemaya, Nethania, Zebadia, Asaheli, Shemiramothi, Yehonathani, Adoniya, Tobia na Tob-adoniya; na makuhani walikuwa Elishama na Yehoramu. Walikichukua kitabu cha sheria ya Mwenyezi-Mungu, wakazunguka nacho katika miji yote ya Yuda wakifundisha watu. Mwenyezi-Mungu alizitia hofu falme zote jirani na Yuda, zikaogopa kupigana vita na Yehoshafati. Baadhi ya Wafilisti walimletea Yehoshafati zawadi pamoja na fedha nyingi, na Waarabu wengine nao wakamletea kondoo madume 7,700, na mabeberu 7,700. Kwa hiyo Yehoshafati aliendelea kuwa mkuu zaidi. Alijenga ngome na miji yenye ghala, kwa hiyo alikuwa na ghala kubwa katika miji ya Yuda. Huko Yerusalemu, aliweka askari wa jeshi mashujaa. Hii ndiyo orodha yao kulingana na koo za baba zao: Adna alikuwa kamanda wa vikosi vya askari 1,000 wa kabila la Yuda. Chini yake, kulikuwa na askari laki tatu. Wa pili katika cheo alikuwa kamanda Yehohanani, akiwa na askari 280,000, na wa tatu alikuwa Amasia mwana wa Zikri, akiwa na askari mashujaa 200,000. Amasia alijitolea kwa hiari kumtumikia Mwenyezi-Mungu. Kamanda wa vikosi vya askari, waliotoka katika kabila la Benyamini alikuwa Eliada, mtu shupavu, naye alikuwa na askari 200,000, wenye nyuta na ngao. Wa pili alikuwa Yehozabadi, aliyekuwa na askari 180,000 waliojiandaa tayari kwa vita. Watu wote hao walimhudumia mfalme huko Yerusalemu; na zaidi ya hayo, mfalme aliweka askari wengine katika miji ile mingine yenye ngome kote nchini Yuda. Wakati mfalme Yehoshafati wa Yuda alipokuwa amekwisha kuwa mtu tajiri na mwenye heshima, alifanya mpango wa ndoa baina ya jamaa yake, na jamaa ya mfalme Ahabu wa Israeli. Baada ya miaka kadhaa Yehoshafati alikwenda Samaria kumtembelea mfalme Ahabu. Ahabu akamchinjia Yehoshafati kondoo na ng'ombe wengi, kwa heshima yake pamoja na watu waliokuwa pamoja naye, kisha akamshawishi aandamane naye kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi. Ahabu mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati mfalme wa Yuda, “Je, utaandamana nami kwenda kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi?” Naye akajibu, “Naam, mimi niko nawe, pia watu wangu ni watu wako. Tutakuwa pamoja nawe vitani.” Kisha Yehoshafati akaendelea kumwambia mfalme wa Israeli, “Lakini kwanza mwulize Mwenyezi-Mungu shauri.” Basi, Ahabu akaitisha kikao cha manabii wapatao 400, akawauliza, “Je, twende tukaushambulie mji wa Ramoth-gileadi, au nisiende?” Wao wakamjibu, “Nenda! Mungu atakupatia ushindi!” Lakini, Yehoshafati akauliza, “Je, hapa hakuna nabii mwingine wa Mwenyezi-Mungu ambaye twaweza kumwuliza shauri?” Naye mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Yupo bado mmoja, Mikaya mwana wa Imla. Yeye twaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu. Lakini namchukia kwa sababu yeye kamwe hatabiri jambo jema juu yangu, ila mabaya tu.” Yehoshafati akamwambia, “Si vizuri mfalme kusema hivyo.” Basi, Ahabu, mfalme wa Israeli akamwita ofisa mmoja na kumwamuru, “Haraka, nenda ukamlete Mikaya mwana wa Imla.” Wakati huo, mfalme wa Israeli pamoja na Yehoshafati, mfalme wa Yuda, walikuwa wameketi katika viti vyao vya enzi wakikaa kwenye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la kuingilia mjini Samaria nao walikuwa wamevalia mavazi yao ya kifalme. Wakati huo manabii wote walikuwa wakitoa unabii wao mbele yao. Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma, akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Washamu hata kuwaangamiza.’” Hata wale manabii wengine wakatabiri vivyo hivyo wakasema, “Nenda ukaushambulie Ramoth-gileadi, Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.” Wakati huo, yule mjumbe aliyetumwa kwa Mikaya alimwambia, “Manabii wengine wote kwa pamoja wamemtabiria mfalme ushindi; tafadhali nawe pia ufanye kama wao, umtabirie mema.” Lakini Mikaya akamjibu, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, kile atakachoniambia Mungu wangu, ndicho nitakachosema.” Basi, Mikaya alipofika mbele ya mfalme, mfalme akamwuliza, “Je, twende kupigana vitani huko Ramoth-gileadi au nisiende?” Mikaya akajibu, “Nenda ushinde; Mwenyezi-Mungu atawatia mikononi mwako.” Lakini mfalme akamwambia, “Nitakuapisha mara ngapi kwamba kila unaposema nami kwa jina la Mwenyezi-Mungu, ni lazima uniambie ukweli mtupu?” Naye Mikaya akasema, “Niliwaona watu wote wa Israeli wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji. Naye Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi; waache warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.’” Hapo mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia, kamwe hatatabiri jema juu yangu, ila mabaya tu?” Kisha Mikaya akasema: “Haya, sikia neno la Mwenyezi-Mungu: Nilimwona Mwenyezi-Mungu ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lake lote la mbinguni limesimama upande wake wa kulia na wa kushoto. Ndipo Mwenyezi-Mungu akauliza, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu mfalme wa Israeli aende akaangamie huko Ramoth-gileadi?’ Kila mmoja akajibu alivyofikiri. Kisha, pepo mmoja akajitokeza mbele ya Mwenyezi-Mungu, akasema, ‘Mimi nitamshawishi.’ Mwenyezi-Mungu akamwuliza, ‘Kwa mbinu gani?’ Naye akajibu, ‘Nitakwenda na kuwafanya manabii wake wote waseme uongo.’ Mwenyezi-Mungu akamwambia, ‘Wewe utamshawishi na utafaulu; haya nenda ukafanye hivyo.’ Basi ndivyo ilivyo: Mwenyezi-Mungu amewafanya hawa manabii wako waseme uongo. Lakini Bwana amenena mabaya juu yako!” Hapo nabii Sedekia mwana wa Kenaana akamkaribia Mikaya, akampiga kofi shavuni na kumwuliza, “Kwa njia gani Roho wa Mwenyezi-Mungu ameniacha na akaja kunena nawe?” Mikaya akamjibu, “Siku ile utakapoingia katika chumba cha ndani kujificha ndipo utakapojua.” Naye mfalme wa Israeli akatoa amri, “Mkamateni Mikaya mrudisheni kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoashi, mwana wa mfalme. Waambie wamfunge gerezani na kumlisha mkate kidogo na maji, mpaka nitakaporudi salama.” Ndipo Mikaya aliposema, “Ukirudi salama, basi, utajua Mwenyezi-Mungu hakunena nami.” Kisha akaendelea kusema, “Sikieni, enyi watu wote!” Basi, mfalme wa Israeli akaenda pamoja na Yehoshafati mfalme wa Yuda kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Mimi nitavaa mavazi yasiyo ya kifalme kuingia vitani, lakini wewe utavaa mavazi yako ya kifalme.” Hivyo mfalme wa Israeli akaenda vitani bila kuvaa mavazi ya kifalme. Mfalme wa Aramu alikuwa amewaamuru makapteni wake waliosimamia magari yake ya kukokotwa akisema, “Msipigane na mtu yeyote yule mkubwa au mdogo, ila tu na mfalme wa Israeli.” Baadaye makapteni hao walipomwona Yehoshafati, walisema, “Huyu mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo, walimwelekea kumshambulia; lakini Yehoshafati akapiga kelele, na Mwenyezi-Mungu akamwokoa. Mungu akawaondoa wale waliokuwa karibu kumshambulia. Makapteni walipotambua kwamba hakuwa mfalme wa Israeli, waliacha kumshambulia, wakarudi. Lakini askari mmoja wa Aramu akauvuta upinde wake kwa kubahatisha, mshale ukamchoma mfalme wa Israeli katika nafasi ya kuungana kwa vazi lake la chuma. Hapo Ahabu akamwambia dereva wa gari lake, “Nimejeruhiwa! Geuza gari uniondoe vitani.” Nayo mapigano siku hiyo, yakazidi kuwa makali huku mfalme wa Israeli amejiegemeza mwenyewe garini akiwaelekea Washamu mpaka jioni. Halafu mnamo machweo ya jua, alifariki. Mfalme Yehoshafati wa Yuda alirejea salama katika ikulu yake mjini Yerusalemu. Lakini mwonaji Yehu mwana wa Hanani, alikwenda kumlaki mfalme, akamwambia, “Je, unadhani ni vema kuwasaidia waovu na kuwapenda wamchukiao Mwenyezi-Mungu? Mambo uliyofanya yamekuletea ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Walakini, kuna wema fulani ndani yako. Umekwisha ziondoa sanamu zote za Ashera, mungu wa kike, na umejitahidi sana kumtafuta Mungu kwa moyo wote.” Mfalme Yehoshafati alikaa Yerusalemu, lakini hata hivyo, mara kwa mara aliwatembelea watu wa Beer-sheba kusini, mpaka milima ya Efraimu, upande wa kaskazini. Alifanya hivyo ili kuwavutia watu wamrudie Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. Aliteua waamuzi katika miji yote ya Yuda yenye ngome, akawaambia, “Muwe waangalifu sana wakati mnapoamua, kwa maana hukumu mtoayo hamwitoi kwa amri ya binadamu, bali kwa amri itokayo kwa Mwenyezi-Mungu, naye yu pamoja nanyi mnapotoa uamuzi. Basi, sasa mwogopeni Mwenyezi-Mungu, muwe waangalifu katika kila jambo mtakalotenda kwa sababu Mwenyezi-Mungu wetu hatavumilia upotoshaji wa haki, wala upendeleo wala ulaji rushwa.” Mjini Yerusalemu, Yehoshafati aliteua Walawi kadhaa, waamuzi na baadhi ya wakuu wa jamaa za Waisraeli wawe waamuzi wa magomvi yahusuyo uvunjaji wa sheria za Mwenyezi-Mungu, au ugomvi baina ya wakazi wa mji. Akawaamuru akisema; “Tekelezeni wajibu wenu mkimwogopa Mwenyezi-Mungu, kwa uaminifu na kwa moyo wote. Kila mara ndugu zenu kutoka katika mji wowote ule wanapowaletea shtaka lolote kuhusu uuaji, uvunjaji wa sheria, amri, kanuni au maagizo, washaurini vema ili wasije wakamkosea Mwenyezi-Mungu. Msipofanya hivyo, nyinyi pamoja na ndugu zenu mtapatwa na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Lakini mkiutekeleza wajibu wenu, hamtakuwa na hatia. Amaria, kuhani mkuu, ndiye atakayesimamia mambo yote yanayomhusu Mwenyezi-Mungu, naye Zebadia mwana wa Ishmaeli, gavana wa Yuda atasimamia mambo yote ya utawala, na Walawi watakuwa maofisa. Jipeni moyo muyatekeleze masharti haya, naye Mwenyezi-Mungu awe pamoja nao walio wema.” Baada ya muda, majeshi ya Moabu na Amoni pamoja na baadhi ya Wameuni, waliivamia Yuda. Watu kadhaa walikuja wakamwambia mfalme Yehoshafati, “Jeshi kubwa limekuja kukushambulia kutoka Edomu, ngambo ya Bahari ya Chumvi. Tayari wamekwisha teka Hasason-tamari.” (Hili ni jina lingine la Engedi). Yehoshafati akashikwa na woga, akamwomba Mwenyezi-Mungu amwongoze. Akatangaza watu wote nchini Yuda wafunge. Watu wakaja Yerusalemu kutoka miji yote ya Yuda, wakakusanyika ili kumwomba Mwenyezi-Mungu awasaidie. Yehoshafati akasimama katikati ya kusanyiko la watu wa Yuda na Yerusalemu mbele ya ua mpya wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaomba kwa sauti akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zetu, wewe ndiwe Mungu uliye mbinguni! Wewe unazitawala falme zote duniani; unao uwezo na nguvu, wala hakuna awezaye kukupinga. Ni wewe ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii wakati watu wako Israeli walipoingia katika nchi hii, ukawapa wazawa wa Abrahamu rafiki yako, iwe yao milele. Nao wamekaa humu, na kukujengea hekalu kwa heshima ya jina lako, wakijua kwamba wakipatwa na maafa yoyote, vita, maradhi mabaya, au njaa, basi watakuja na kusimama mbele ya nyumba hii mbele yako, wakulilie katika shida zao, nawe utawasikiliza na kuwaokoa. Sasa watu wa Amoni, Moabu na wa mlima Seiri, ambao hukuwaruhusu babu zetu washambulie nchi zao walipotoka Misri, wakapitia kandokando wasiwaangamize, tazama, jinsi wanavyotulipa. Wanakuja kututoa katika nchi yako uliyotupa iwe mali yetu. Wewe ndiwe Mungu wetu! Waadhibu, kwani sisi hatuna uwezo wowote mbele ya jeshi kubwa kama hili linalotujia. Hatujui la kufanya ila tunatazamia msaada kutoka kwako.” Wanaume wote wa Yuda, pamoja na wake zao na watoto wao, walikuwa wamesimama hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu. Ndipo Roho wa Mwenyezi-Mungu akamjia mmoja wa Walawi aliyekuwa hapo, jina lake Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, wa ukoo wa Asafu. Yahazieli akasema, “Sikilizeni watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu na mfalme Yehoshafati, Mwenyezi-Mungu awaambia hivi: Msiogope wala msihangaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu. Kesho washambulieni wakati watakapokuwa wakipanda Bonde la Sisi. Mtawakuta mwisho wa bonde, mashariki mwa jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita hivi. Nyinyi jipangeni tu halafu mngojee, na mtaona Mwenyezi-Mungu akiwashinda kwa niaba yenu. Enyi watu wa Yuda na Yerusalemu, msiogope wala msifadhaike. Nendeni vitani, naye Mwenyezi-Mungu atakuwa pamoja nanyi!” Hapo mfalme Yehoshafati akasujudu pamoja na watu wote wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu wakamsujudu na kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Walawi wa ukoo wa Kohathi na Kora, wakasimama na kumsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sauti kubwa sana. Kesho yake, wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda mpaka katika jangwa la Tekoa. Walipokuwa wanaondoka, Yehoshafati alisimama, akawaambia, “Nisikilizeni, enyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu! Mwaminini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nanyi mtakuwa imara. Muwe na imani na manabii wake, nanyi mtafaulu.” Baada ya kushauriana na watu, mfalme alichagua wanamuziki fulani, akawaagiza wajivike mavazi yao rasmi kisha watangulie mbele ya jeshi, wakiimba: “Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, maana fadhili zake zadumu milele!” Wakati walipoanza kuimba na kusifu, Mwenyezi-Mungu aliwavuruga akili wanajeshi wa Amoni, Moabu na wa Mlima Seiri waliokuja kupigana na Yuda. Na wanajeshi hao wakashindwa. Watu wa Amoni na wa Moabu wakawashambulia wenyeji wa mlima Seiri, na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kuwaangamiza wakazi wa mlima Seiri wakaanza kushambuliana wao kwa wao, wakaangamizana. Jeshi la Yuda lilipofika penye mnara wa ulinzi huko jangwani, waliangalia upande wa maadui, wakaona maiti zimetapakaa kila mahali. Hakuna mtu yeyote aliyenusurika. Yehoshafati na wanajeshi wake wakaenda kuchukua nyara wakakuta ng'ombe wengi, mali, nguo na vitu vingine vya thamani. Iliwachukua muda wa siku tatu kusomba nyara hizo, na hata hivyo, hawakuzimaliza kwani zilikuwa nyingi mno. Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Sifa, na kumsifu Mwenyezi-Mungu kwa yote aliyowafanyia. Ndio maana bonde hilo linaitwa Bonde la Sifa hadi hivi leo. Kisha Yehoshafati akawaongoza wanajeshi wake mpaka Yerusalemu kwa shangwe, kwa sababu Mwenyezi-Mungu aliwashinda maadui zao. Walipofika Yerusalemu, walikwenda moja kwa moja hadi nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakipiga vinanda, vinubi na tarumbeta. Falme zote ziliingiwa na hofu ziliposikia jinsi Mwenyezi-Mungu alivyowashinda maadui za Israeli. Basi, Yehoshafati akatawala kwa amani, na Mungu akampa amani pande zote. Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala Yuda. Alitawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na mitano. Mama yake alikuwa Azuba binti Shilhi. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyofanya Asa baba yake. Lakini hakupaharibu mahali pa kutolea tambiko kilimani. Watu walikuwa bado hawajamgeukia na kumwabudu Mungu wa babu zao kwa mioyo yao. Matendo mengine ya Yehoshafati, kutoka mwanzo wa utawala wake mpaka mwisho, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za Yehu mwana wa Hanani, ambamo zimo katika kitabu cha Wafalme wa Israeli. Baada ya haya, Yehoshafati mfalme wa Yuda, alijiunga na Ahazia mfalme wa Israeli, aliyetenda mambo maovu. Walishirikiana kuunda merikebu za kusafiria mpaka Tarshishi; waliziundia huko Esion-geberi. Lakini Eliezeri mwana wa Dodavahu, kutoka mji wa Maresha, akatoa unabii dhidi ya Yehoshafati, akisema, “Kwa sababu umejiunga na Ahazia, Mwenyezi-Mungu atavunja merikebu zote mlizotengeneza.” Baadaye merikebu hizo zilivunjikavunjika; kwa hiyo hazikuweza kusafiri mpaka Tarshishi. Hatimaye Yehoshafati alifariki na kuzikwa pamoja na babu zake katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi; naye Yehoramu mwanawe akatawala mahali pake. Yehoramu alikuwa na ndugu kadhaa wana wa Yehoshafati: Azaria, Yehieli, Zekaria, Azaria, Mikaeli na Shefatia. Baba yao aliwapa zawadi kubwakubwa za fedha, dhahabu na vitu vingine vya thamani, na pia miji ya Yuda yenye ngome. Lakini kwa sababu Yehoramu ndiye aliyekuwa mzaliwa wake wa kwanza, Yehoshafati akampa ufalme atawale badala yake. Yehoramu alipokikalia kiti cha enzi na utawala wake ulipokuwa umekwisha imarika, yeye aliwaua ndugu zake wote kwa upanga, na pia baadhi ya wakuu wa Israeli. Yehoramu alianza kutawala akiwa na umri wa miaka thelathini na miwili. Alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka minane. Alizifuata njia mbaya za mfalme Ahabu na za wafalme wengine wa Israeli kama jamaa ya Ahabu ilivyofanya kwa sababu mkewe alikuwa binti ya Ahabu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini Mwenyezi-Mungu hakutaka kuangamiza ukoo wa Daudi kwa ajili ya agano alilokuwa amefanya na Daudi na pia kwa sababu alikuwa ameahidi wazawa wake wataendelea kutawala milele. Wakati wa enzi ya Yehoramu, watu wa Edomu waliasi utawala wa Yuda, wakamtawaza mfalme wao wenyewe. Kwa hiyo, Yehoramu pamoja na makamanda wake na magari yake yote aliondoka akawashambulia Waedomu waliokuwa wamemzunguka yeye pamoja na makamanda wake na magari. Hivyo Edomu imeuasi utawala wa Yuda mpaka sasa. Wakati huohuo pia, wakazi wa Libna nao wakauasi utawala wake kwa sababu Yehoramu alikuwa amemwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake. Isitoshe, alitengeneza mahali pa kuabudia miungu mingine katika milima ya Yuda na kusababisha wakazi wa Yerusalemu kukosa uaminifu na watu wa Yuda kupotoka. Nabii Elia alimpelekea mfalme Yehoramu barua ifuatayo: “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Daudi babu yako, anakulaani kwa sababu hukufuata mwenendo wa Yehoshafati baba yako, au wa Asa mfalme wa Yuda. Badala yake umeifuata mienendo ya wafalme wa Israeli na kuwaongoza watu wa Yuda na Yerusalemu katika kukosa uaminifu kama vile Ahabu, na wafalme wa jamaa yake waliomfuata walivyowaongoza watu wa Israeli kukosa uaminifu. Pia umewaua ndugu zako, ndugu za baba mmoja waliokuwa watu wema zaidi kuliko wewe. Kwa sababu hiyo, Mwenyezi-Mungu atawaadhibu vikali watu wako, wanao, wake zako na kuiharibu mali yako yote. Wewe mwenyewe utaugua maradhi mabaya ya tumbo, ambayo yataongezeka siku hata siku, mpaka matumbo yako yatoke nje.” Kulikuwa na Wafilisti na Waarabu wengine waliokuwa wakikaa karibu na Waethiopia. Hawa, Mwenyezi-Mungu aliwapandisha hasira ili wapigane na Yehoramu. Basi, wakaishambulia nchi ya Yuda, wakaiteka mali yote iliyokuwamo katika jumba la mfalme na kuwachukua mateka wanawe wote na wake zake, isipokuwa Ahazia, mwanawe mdogo. Baada ya haya yote, Mwenyezi-Mungu akamletea mfalme ugonjwa wa tumbo usioponyeka. Aliendelea kuugua, na ugonjwa wake ukawa unaongezeka siku hata siku, hata kufikia mwisho wa mwaka wa pili, akafariki dunia katika maumivu makali. Watu hawakuwasha moto kuomboleza kifo chake kama walivyowafanyia babu zake. Yehoramu alianza kutawala akiwa na umri wa miaka thelathini na miwili; akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka minane. Wakati alipofariki, hakuna mtu yeyote aliyemsikitikia. Alizikwa katika mji wa Daudi, ila si katika makaburi ya wafalme. Wakazi wa Yerusalemu walimpa Ahazia, mwana mdogo wa Yehoramu, ufalme, atawale mahali pa baba yake kwa sababu wakubwa wake wote waliuawa na kikundi fulani kilichokuja kambini pamoja na Waarabu. Hivyo, Ahazia mwana wa Yehoramu, mfalme wa Yuda, akatawala. Ahazia, alianza kutawala akiwa mwenye umri wa miaka arubaini na miwili, akatawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri. Kwa sababu mama yake alikuwa mshauri wake katika kutenda maovu, naye pia alifuata mienendo ya jamaa ya Ahabu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile jamaa ya Ahabu ilivyofanya kwani hao ndio waliokuwa washauri wake baada ya kifo cha baba yake, hata aangamie. Hata alifuata shauri lao, akaenda pamoja na mfalme Yehoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli kupigana na Hazaeli mfalme wa Shamu huko Ramoth-gileadi. Nao Washamu walimjeruhi Yoramu. Kisha akarudi Yezreeli ili apate kutibiwa majeraha aliyoyapata huko Rama, wakati alipopigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alimtembelea Yoramu mwana wa Ahabu huko Yezreeli kwa sababu alikuwa mgonjwa. Lakini hiyo ilikuwa imepangwa na Mungu kuwa maangamizi yampate Ahazia kwa njia hiyo ya kumtembelea Yoramu. Maana alipofika huko, alitoka pamoja na Yoramu kwenda kupigana na Yehu mwana wa Nimshi ambaye Mwenyezi-Mungu alimteua kuuangamiza uzao wa Ahabu. Wakati Yehu alipokuwa akiwahukumu jamaa ya Ahabu alikutana na wakuu wa Yuda pamoja na wana wa ndugu zake Ahazia, waliomtumikia Ahazia, akawaua. Alimtafuta Ahazia, naye akakamatwa akiwa amejificha huko Samaria. Walimleta hadi kwa Yehu, akauawa. Waliuzika mwili wake kwani walisema, “Yeye ni mjukuu wa Yehoshafati, ambaye alimtafuta Mwenyezi-Mungu kwa moyo wake wote.” Hapakubaki hata mtu mmoja wa jamaa ya Ahazia ambaye angeweza kuwa falme. Mara Athalia, mamake Ahazia, alipoona kuwa mwanawe ameuawa, alitoka akaangamiza jamii yote ya kifalme ya Yuda. Lakini Yehosheba, binti ya mfalme Yehoramu alimchukua Yoashi, akamtwaa kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Alimficha yeye pamoja na yaya wake, katika chumba cha kulala. Hivyo Yehosheba, binti ya mfalme Yehoramu, mke wa kuhani Yehoadani, kwa sababu alikuwa dadaye Ahazia, alimficha Yoashi ili Athalia asimuue. Naye alikaa nao kwa muda wa miaka sita akiwa amefichwa ndani ya nyumba ya Mungu wakati Athalia alipokuwa akitawala nchi. Baadaye, mnamo mwaka wa saba, kuhani Yehoyada alijipa moyo akafanya mapatano na makapteni: Azaria mwana wa Yehoramu, Ishmaeli mwana wa Yehohanani, Azaria mwana wa Obedi, Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri. Wakazunguka katika miji yote ya Yuda wakiwakusanya Walawi na viongozi wa makabila ya Israeli, wakaenda mpaka Yerusalemu. Mkutano wote ukafanya agano na mfalme katika nyumba ya Mungu. Yehoyada akawaambia, “Mwangalie huyu mwana wa mfalme! Mwacheni atawale kulingana na ahadi aliyoitoa Mwenyezi-Mungu kuhusu uzao wa Daudi. Hivi ndivyo mtakavyofanya: Theluthi moja yenu nyinyi makuhani na Walawi mtakaoshika zamu siku ya Sabato, mtayalinda malango, theluthi nyingine italinda ikulu na theluthi iliyobakia mtalinda Lango la Msingi. Watu wote watakuwa katika nyua za nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Asikubaliwe mtu mwingine yeyote kuingia nyumba ya Mwenyezi-Mungu isipokuwa makuhani tu pekee na wale Walawi watakaokuwa wanahudumu. Hao wanaweza kuingia kwa sababu wao ni watakatifu, lakini wale watu wengine wote, watatii amri ya Mwenyezi-Mungu. Walawi watamzunguka mfalme, kila mtu na silaha yake mkononi; na mtu yeyote atakayejaribu kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, atauawa. Mkae na mfalme popote aendapo.” Walawi na watu wa Yuda walitii amri zote alizotoa kuhani Yehoyada. Kila ofisa akawachukua watu wake wote, wale waliokuwa wamemaliza zamu na wale waliokuwa wanaingia kushika zamu siku ya Sabato; kwa sababu Yehoyada hakuwaruhusu waondoke. Kisha kuhani Yehoyada akawapa makapteni mikuki na ngao kubwa na ndogo zilizokuwa mali ya mfalme Daudi, na ambazo zilikuwa zimewekwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kisha, akawapanga watu wote kuanzia upande wa kusini mpaka upande wa kaskazini wa nyumba na kuzunguka madhabahu na nyumba, kila mmoja silaha yake mkononi, ili kumlinda mfalme. Halafu wakamtoa nje mwana wa mfalme, wakamvika taji kichwani, na kumpa ule ushuhuda; wakamtawaza nao Yehoyada na wanawe wakampaka mafuta awe mfalme, kisha watu wakashangilia wakisema, “Aishi mfalme!” Naye Malkia Athalia aliposikia sauti za watu wakikimbia na kumshangilia mfalme aliwaendea hao watu waliokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Alipochungulia akamwona mfalme mpya amesimama karibu na nguzo kwenye lango, huku makapteni na wapiga tarumbeta wakiwa kando ya mfalme na wakazi wote wakishangilia na kupiga tarumbeta; nao waimbaji wakiwa na ala zao za muziki wakiongoza watu katika sherehe; ndipo aliporarua nguo zake na kusema kwa sauti kubwa “Uhaini! Uhaini!” Kisha kuhani Yehoyada aliwatoa nje makapteni wa jeshi akisema mtoeni nje katikati ya askari; yeyote atakayemfuata na auawe kwa upanga. Kwa sababu alisema “Msimuulie katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Basi, wakamkamata, na akaingia katika njia ya Lango la Farasi la ikulu, wakamuulia huko. Yehoyada akafanya agano kati yake mwenyewe, watu wote, na mfalme kwamba watakuwa watu wa Mwenyezi-Mungu. Halafu watu wote wakaenda kwenye nyumba ya Baali, wakaibomoa na kuzivunja madhabahu pamoja na sanamu zake. Kisha wakamuua Matani, kuhani wa Baali, mbele ya madhabahu. Kuhani Yehoyada akaweka walinzi kulinda nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hao walinzi walisimamiwa na makuhani na Walawi ambao Daudi aliwaweka katika huduma ya kutunza nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kutoa sadaka za kuteketezwa kwa Mwenyezi-Mungu kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, wakishangilia na kuimba kwa kufuata amri ya Daudi. Aliweka mabawabu malangoni mwa nyumba ya Mwenyezi-Mungu ili asije akaingia mtu yeyote aliye najisi kwa namna moja au nyingine. Aliwachukua makapteni wa jeshi, waheshimiwa, watawala wa watu, na wakazi wote; nao wakamsindikiza mfalme kutoka nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakapitia katika lango la juu mpaka ikulu. Kisha wakamkalisha mfalme kwenye kiti cha enzi. Kwa hiyo wakazi wote walishangilia; na mji wote ulikuwa mtulivu baada ya Athalia kuuawa kwa upanga. Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka arubaini huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Sibia kutoka Beer-sheba. Wakati wote kuhani Yehoyada alipokuwa hai Yoashi alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu. Yehoyada akamwoza wake wawili, nao wakamzalia watoto wa kiume na wa kike. Baadaye Yoashi aliamua kurekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Basi, akawaita makuhani na Walawi na kuwaamuru, “Nendeni katika miji ya Yuda, mkusanye fedha kutoka kwa Waisraeli wote ili kurekebisha nyumba ya Mungu wenu kila mwaka; harakisheni.” Lakini Walawi hawakuharakisha. Basi, mfalme akamwita kiongozi Yehoyada, akamwuliza, “Mbona hujaamrisha Walawi kukusanya kutoka kwa watu wa Yuda na Yerusalemu, kodi ambayo Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliagiza watu walipe kwa ajili ya Hema Takatifu la Mwenyezi-Mungu?” (Athalia yule mwanamke mwovu na wafuasi wake walivunja nyumba ya Mungu na kuingia ndani; na vyombo vitakatifu vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu walivitumia katika ibada za Mabaali.) Basi, mfalme aliwaamuru Walawi, wakatengeneza sanduku la matoleo na kuliweka nje ya lango la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kisha tangazo likatolewa kote katika Yuda na Yerusalemu, kwamba watu wote wamletee Mwenyezi-Mungu kodi ambayo Mose mtumishi wa Mungu, aliwaamuru Waisraeli walipokuwa jangwani. Wakuu wote na watu wote walifurahi wakaleta kodi yao wakaitumbukiza kwenye sanduku mpaka walipomaliza kufanya hivyo. Walawi walipopeleka sanduku hilo kwa maofisa wa mfalme, nao walipoona kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha ndani, katibu wa mfalme pamoja na mwakilishi wa kuhani mkuu, walizitoa sandukuni, kisha wakalirudisha mahali pake. Waliendelea kufanya hivyo kila siku, wakakusanya fedha nyingi. Mfalme na Yehoyada walizitoa fedha hizo na kuwapa wale waliosimamia kazi ya urekebishaji wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao wakawaajiri waashi, maseremala warekebishe nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Waliajiri pia mafundi wa chuma na shaba ili kurekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hivyo mafundi hao walishughulika na kazi hiyo kwa bidii, wakairudisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu katika hali yake ya awali, wakaiimarisha. Walipomaliza kuitengeneza nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walimletea mfalme na Yehoyada dhahabu na fedha iliyobaki; halafu vyombo kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu vilitengenezwa kwa fedha hizo, vyombo hivyo vilikuwa vya kutumika katika huduma ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, matoleo ya sadaka za kuteketeza na mabakuli ya kufukizia ubani, pia vyombo vya dhahabu na vya fedha. Watu waliendelea kutoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakati wote wa utawala wa Yehoyada. Lakini Yehoyada alizeeka na alipofikisha umri wa miaka 130, alifariki. Wakamzika katika mji wa Daudi, kwenye makaburi ya wafalme ili kuonesha heshima yao kwake kwa sababu alifanya mema katika Israeli kwa ajili ya Mungu na nyumba yake. Baada ya kifo cha Yehoyada, wakuu wa Yuda walimjia mfalme Yoashi wakamsujudia, wakamshawishi, naye akakubaliana nao. Basi, watu wakaacha kuabudu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, wakaanza kuabudu Maashera na sanamu. Ghadhabu ya Mungu iliwaka juu ya Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hatia hii. Hata hivyo, aliwapelekea manabii kuwaonya ili wamrudie Mwenyezi-Mungu, lakini wao hawakuwasikiliza. Ndipo Roho ya Mungu ikamjia Zekaria mwana wa kuhani Yehoyada, naye akasimama mbele ya watu mahali palipokuwa juu kidogo, akawaambia, “Mwenyezi-Mungu aliwaulizeni kwa nini mnazivunja amri zake na sasa hamwezi kufanikiwa! Kwa vile mmemwacha, naye pia amewaacha!” Lakini wakamfanyia njama; na kwa amri ya mfalme, wakampiga mawe kwenye ua wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakamuua. Mfalme Yoashi aliyasahau mema yote aliyotendewa na Yehoyada, baba yake Zekaria, akamuua mwanawe. Alipokuwa anakufa, alisema, “Mwenyezi-Mungu na ayaone matendo yenu, akalipize kisasi.” Mwishoni mwa mwaka, jeshi la Washamu lilishambulia Yerusalemu na Yuda. Waliwaua wakuu wote, wakateka nyara nyingi na kumpelekea mfalme wa Damasko. Hata ingawa jeshi la Shamu lilikuwa dogo, Mwenyezi-Mungu alilipa ushindi dhidi ya jeshi kubwa la watu wa Yuda kwa sababu hao watu wa Yuda walikuwa wamemwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. Hivyo, Washamu wakatekeleza adhabu ya Mungu juu ya mfalme Yoashi. Maadui walipoondoka, walimwacha akiwa amejeruhiwa vibaya sana, maofisa wake wakala njama wakamwulia kitandani mwake, kulipiza kisasi mauaji ya mwana wa kuhani Yehoyada. Alizikwa katika mji wa Daudi, lakini si kwenye makaburi ya wafalme. Watu waliomfanyia njama walikuwa Zabadi mwana wa mwanamke Mwamoni jina lake Shimeathi, na Yehozabadi mwana wa mwanamke Mmoabu jina lake Shimrithi. Habari za wanawe Yoashi za kuirekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu na unabii wote juu yake, zimeandikwa katika Maelezo ya Kitabu cha Wafalme. Amazia mwanawe alitawala baada yake. Amazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, akatawala kwa muda wa miaka ishirini na mitano katika Yerusalemu. Mama yake aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu. Alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu ingawa hakuyatenda kwa moyo mnyofu. Mara tu Amazia alipojiimarisha mamlakani aliwaua watumishi waliomuua mfalme baba yake. Lakini hakuwaua watoto wao, kama ilivyoandikwa katika sheria zilizomo katika kitabu cha Mose, ambapo Mwenyezi-Mungu anasema: “Wazazi hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya wazazi wao; bali kila mtu atauawa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.” Mfalme Amazia aliwakusanya wanaume wa makabila ya Yuda na Benyamini, akawapanga katika vikosi mbalimbali kulingana na koo zao, akawaweka chini ya makamanda wa maelfu na wa mamia. Alipowakagua wale wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, alipata jumla ya watu 300,000. Wote walikuwa watu wateule, tayari kwa vita, hodari wa kutumia mikuki na ngao. Tena, alikodisha askari wengine mashujaa 1,000 kutoka Israeli, kwa gharama ya kilo 3,000 za fedha. Lakini mtu wa Mungu alimwendea, akamwambia, “Ee mfalme, usiende vitani pamoja na hawa askari wa Israeli, maana Mwenyezi-Mungu hayuko pamoja na watu wa Israeli. Hayuko pamoja na hawa Waefraimu wote. Bali, hivyo, hata ukiwa hodari vitani, Mungu atakufanya ushindwe na maadui, kwa kuwa Mungu ana nguvu kumpa binadamu ushindi au kumfanya binadamu ashindwe.” Amazia akamwuliza huyo mtu wa Mungu, “Tutafanyaje na fedha yote ambayo nimekwisha wapa wanajeshi wa Israeli?” Naye akamjibu, “Mwenyezi-Mungu anaweza kukupa zaidi ya hiyo.” Hapo Amazia akawaachia wanajeshi waliotoka Efraimu warudi makwao. Basi wakarejea kwao wakiwa wamewakasirikia sana watu wa Yuda. Amazia alijipa moyo akaliongoza jeshi lake hadi Bonde la Chumvi. Hapo akapigana na kuwaua watu 10,000 wa Seiri. Waliteka watu 10,000, wakawapandisha juu ya jabali na kuwatupa chini miambani, wakapondeka vipandevipande. Wakati huohuo, wale wanajeshi Waisraeli ambao Amazia aliwaachia warudi kwao akiwakataza wasiandamane naye vitani, walikwenda na kuishambulia miji ya Yuda, toka Samaria hadi Beth-horoni, wakaua watu 3,000 na kuteka nyara nyingi. Amazia aliporejea baada ya kuwashinda Waedomu, alileta miungu ya Waedomu akaifanya kuwa miungu yake, akaisujudia na kuifukizia ubani. Haya yalimkasirisha sana Mwenyezi-Mungu, akatuma nabii kwa Amazia. Nabii huyo akamwuliza Amazia, “Kwa nini unategemea miungu ya watu wengine ambayo hata haikuweza kuwaokoa watu wake wenyewe kutoka mikononi mwako?” Lakini hata kabla hajamaliza kusema, Amazia alimkata kauli akamwambia, “Nyamaza! Tulikufanya lini mshauri wa mfalme? Wataka kuuawa?” Nabii akanyamaza, lakini akasema, “Ninafahamu kuwa Mungu ameamua kukuangamiza kwa maana umetenda haya yote, kisha unapuuza shauri langu.” Basi, Amazia mfalme wa Yuda alifanya shauri, akatuma ujumbe kwa Yehoashi, mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu mfalme wa Israeli, akamwambia, “Njoo tupambane.” Lakini Yoashi mfalme wa Israeli alimpelekea ujumbe Amazia akisema, “Siku moja, mchongoma wa Lebanoni uliuambia mwerezi wa hukohuko Lebanoni, ‘Mwoze binti yako kwa mwanangu!’ Lakini mnyama mmoja wa mwituni akapita hapo na kuukanyagakanyaga mchongoma huo. Sasa wewe Amazia unasema, ‘Nimewaua Waedomu;’ na moyo unakufanya ujivune. Basi, kaa nyumbani mwako; ya nini kujitafutia taabu zitakazokuangamiza wewe mwenyewe pamoja na watu wako wa Yuda?” Lakini Amazia hakujali kwa kuwa lilikuwa kusudi la Mungu ili awaweke mkononi mwa maadui zao kwa sababu alitegemea miungu ya Edomu. Kwa hiyo, Yehoashi, mfalme wa Israeli alitoka akakabiliana uso kwa uso na Amazia, mfalme wa Yuda, huko vitani Beth-shemeshi, nchini Yuda. Watu wa Yuda walishindwa na watu wa Israeli na kila mmoja alirudi nyumbani kwake. Halafu Yehoashi mfalme wa Israeli alimteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia huko Beth-shemeshi, akampeleka hadi Yerusalemu. Huko, aliubomoa ukuta wa mji huo, kuanzia Lango la Efraimu mpaka Lango la Pembeni, umbali wa karibu mita 200. Alichukua dhahabu yote na fedha hata na vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu chini ya ulinzi wa Obed-edomu; pia alichukua hazina ya ikulu na mateka kisha akarudi Samaria. Amazia mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya kifo cha mfalme Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli. Matendo mengine yote ya Amazia kutoka mwanzo hadi mwisho yameandikwa katika Kitabu cha Habari za Wafalme wa Yuda na Israeli. Njama za kumuua Amazia zilifanywa Yerusalemu tangu alipomwacha Mwenyezi-Mungu, kwa hiyo alikimbilia Lakishi. Lakini maadui walituma watu Lakishi wakamuua huko. Maiti yake ililetwa juu ya farasi, na kuzikwa kwenye makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi. Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Uzia mwanawe Amazia akiwa mwenye umri wa miaka kumi na sita, wakamtawaza mahali pa Amazia baba yake. Halafu baada ya kifo cha baba yake aliujenga upya mji wa Elothi na kuurudisha kwa Yuda. Uzia alianza kutawala akiwa na umri wa miaka kumi na sita; akatawala kwa muda wa miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Yekolia wa Yerusalemu. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama baba yake. Alimtumikia Mwenyezi-Mungu kwa uaminifu wakati wa kuishi kwa Zekaria, aliyemfundisha kumtii Mungu. Kadiri alivyomtafuta Mungu, Mungu alimfanikisha. Uzia aliondoka akapiga vita dhidi ya Wafilisti, akazibomoa kuta za miji ya Gathi, Yabne na Ashdodi. Akajenga miji katika eneo la Ashdodi na kwingineko nchini Filistia. Mungu alimsaidia kuwashinda Wafilisti, Waarabu waliokaa Gurbaali na Wameuni. Waamoni walimlipa kodi, na sifa zake zikaenea hadi Misri, kwa sababu alipata nguvu. Tena Uzia alijenga minara katika Yerusalemu penye Lango la Pembeni, Lango la Bondeni na Pembeni na kuiimarisha. Hata nyikani pia alijenga minara, akachimba mabwawa mengi, maana alikuwa na mifugo mingi kwenye sehemu za miinuko na tambarare. Alikuwa na wakulima wa watunza mizabibu milimani, na katika ardhi yenye rutuba kwani alipenda kilimo. Zaidi ya hayo, Uzia alikuwa na jeshi lililojiandaa tayari kwa vita. Lilikuwa limegawanywa katika vikosi mbalimbali, na orodha yao iliwekwa na katibu Yeieli, na Maaseya, ofisa, nao wote walikuwa chini ya uongozi wa Hanania, mmoja wa makamanda wake mfalme. Jumla, viongozi wote wa majeshi walikuwa 2,600. Chini yao, kulikuwa na jeshi la askari 307,500, wenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na adui yeyote wa mfalme. Uzia aliwapa askari hao ngao, mikuki, kofia za chuma, deraya, pinde na mawe kwa ajili ya kupiga kwa kombeo. Huko Yerusalemu mafundi wake walimtengenezea mitambo ya kurushia mishale na mawe makubwamakubwa. Sifa zake zilienea kila mahali, nguvu zake zikaongezeka zaidi kwa sababu ya msaada mwingi alioupata kutoka kwa Mungu. Wakati mfalme Uzia alipokuwa na nguvu, alijaa kiburi ambacho kilisababisha maangamizi yake. Alimwasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wake kwa kuingia hekaluni akikusudia kufukiza ubani madhabahuni. Lakini kuhani Azaria, pamoja na makuhani wengine mashujaa themanini, wakamfuata mfalme na kumzuia. Wakamwambia, “Si wajibu wako hata kidogo Uzia, kumfukizia Mwenyezi-Mungu ubani. Ni makuhani tu wa uzao wa Aroni ambao wamewekwa wakfu kufukiza ubani. Ondoka mahali hapa patakatifu. Umemkosea Mwenyezi-Mungu na hutapata heshima yoyote kutoka kwake.” Wakati huo, Uzia alikuwa amesimama hekaluni karibu na madhabahu, ameshikilia chetezo cha kufukizia ubani mkononi. Aliwakasirikia makuhani; na mara alipofanya hivyo, akashikwa na ukoma katika paji la uso wake mbele ya makuhani hao. Azaria, kuhani mkuu, na wale makuhani wengine, walimtazama, kisha wakaharakisha kumtoa nje; hata yeye mwenyewe akafanya haraka kutoka, kwa maana Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwadhibu. Basi, mfalme Uzia akawa na ukoma mpaka siku ya kufa kwake. Alikaa katika nyumba yake ya pekee kwani hakukubaliwa tena kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Naye Yothamu mtoto wake, akatunza jamaa yake huku akitawala wakazi wa nchi. Matendo mengine yote ya mfalme Uzia kutoka mwanzo mpaka mwisho, yaliandikwa na nabii Isaya mwana wa Amozi. Uzia alifariki na kuzikwa katika eneo la kuzikia wafalme, kwa sababu walisema, “Yeye ana ukoma”. Naye Yothamu mwanawe, akatawala mahali pake. Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, alitawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyofanya Uzia baba yake; isipokuwa yeye hakuingia katika hekalu la Mwenyezi-Mungu nao watu waliendelea kufanya maovu. Yothamu alijenga Lango la Kaskazini la nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kushughulika sana na ujenzi wa ukuta sehemu ya Ofeli. Alijenga miji kwenye nchi ya milima ya Yuda, na kwenye misitu, akajenga ngome na minara katika milima yenye misitu. Alipigana vita dhidi ya mfalme wa Amoni na kuwashinda. Katika mwaka huo Waamoni walimtolea ushuru wa kilo 3,400, tani 1,000 za ngano na kilo 1,000 za shayiri; waliendelea kufanya hivyo katika mwaka wa pili na wa tatu. Mfalme Yothamu aliendelea kuwa mwenye nguvu, kwa sababu aliishi kwa kumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. Matendo mengine ya Yothamu, vita vyake na maongozi yake, yote yameandikwa katika Kitabu cha Habari za Wafalme wa Israeli na Yuda. Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, akatawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu. Alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi. Naye Ahazi mwanawe akatawala mahali pake. Ahazi alianza kutawala akiwa na umri wa miaka ishirini; alitawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu. Yeye, hakufuata mfano mzuri wa Daudi babu yake, bali alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, na kufuata mienendo ya wafalme wa Israeli. Isitoshe, alitengeneza hata sanamu za kusubu za Mabaali, akafukiza ubani kwenye Bonde la mwana wa Hinomu na kuwateketeza wanawe kama tambiko, akiiga desturi za kuchukiza za watu ambao walifukuzwa na Mwenyezi-Mungu wakati Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini. Alitoa tambiko na kufukiza ubani mahali pa kuabudia miungu mingine, vilimani na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, alimwacha mfalme Ahazi ashindwe na mfalme wa Aramu ambaye pia alichukua mateka watu wake wengi, akarudi nao Damasko. Kadhalika, alimfanya ashindwe na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, ambaye alimshinda na kuua watu wengi sana. Aliua askari mashujaa wa Yuda 120,000 katika siku moja. Ilitokea hivyo kwa sababu walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. Zikri, askari mmoja shujaa wa Israeli, alimuua Maaseya, mwana wa mfalme, Azrikamu, kamanda wa Ikulu, na Elkana aliyekuwa mtu wa pili chini ya mfalme. Jeshi la Israeli lilichukua mateka ndugu zao watu laki mbili wakiwemo wanawake na watoto. Waliwachukua hadi Samaria pamoja na mali nyingi waliyoteka nyara. Baadaye kidogo mtu mmoja, jina lake Odedi, nabii wa Mwenyezi-Mungu, alikuwa anakaa Samaria. Yeye alitoka kuwalaki wanajeshi wa Israeli pamoja na mateka wao wa Yuda walipokuwa karibu kuingia Samaria, akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, alikuwa amewakasirikia watu wa Yuda, ndiyo maana akawatia mikononi mwenu lakini mmewaua kwa hasira. Tendo hilo limefika mbinguni. Sasa mnanuia kuwafanya wanaume na wanawake wa Yuda na Yerusalemu watumwa wenu. Je, hamtambui ya kuwa nyinyi pia mmetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu? Sasa sikieni yale nisemayo: Warudisheni ndugu zenu na dada zenu mliowateka, maana ghadhabu kali ya Mwenyezi-Mungu iko juu yenu.” Nao wakuu fulani wa Efraimu, Azaria mwana wa Yohanani, Berekia mwana wa Meshilemothi, Yehizkia mwana wa Shalumu na Amasa mwana wa Hadlai, pia waliwashutumu hao waliotoka vitani. Wakawaambia, “Msiwalete humu mateka hao, kwa sababu mnanuia kutuletea hatia mbele ya Mwenyezi-Mungu; tendo hili huku litakuwa nyongeza ya dhambi yetu na hatia yetu; kwa sababu hatia yetu tayari ni kubwa na kuna ghadhabu kali juu ya Israeli.” Hivyo, wanajeshi waliwaacha mateka wao na nyara zote mbele ya wakuu na mkutano wote. Wale wakuu waliotajwa majina yao waliwachukua mateka na kwa kutumia nyara wakawavika mateka ambao hawakuwa na nguo; waliwapatia ndara, chakula na vinywaji, na kuwapaka mafuta. Wale ambao walikuwa hawajiwezi, wakawabeba kwa punda, wakawachukua mateka wote hadi Yeriko, mji wa mitende, kwa ndugu zao; kisha wao wakarudi Samaria. Wakati huo, mfalme Ahazi alituma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru kuomba msaada, kwa sababu Waedomu walikuwa wamekuja tena, wakaivamia nchi ya Yuda, wakawashinda na kuchukua mateka wengi. Wakati huohuo pia, Wafilisti walikuwa wakiishambulia miji ya Shefela na Negebu ya Yuda. Waliiteka miji ya Beth-shemeshi, Ayaloni, Gederothi, Soko na vijiji vyake, Timna na vijiji vyake, Gimzo na vijiji vyake, wakafanya makao yao huko. Kwa sababu mfalme Ahazi wa Israeli alikuwa na ukatili kwa watu wake, na alikosa uaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu aliwafanya watu wa Yuda wakose nguvu. Tiglath-pileseri, mfalme wa Ashuru alimshambulia badala ya kumtia nguvu. Ahazi alichukua dhahabu kutoka katika nyumba ya Mungu, kutoka ikulu na nyumba za wakuu, akampa mfalme wa Ashuru kama kodi; lakini hili pia halikumsaidia kitu. Wakati alipokuwa taabuni zaidi, mfalme huyu Ahazi alizidi kumwasi Mwenyezi-Mungu. Maana aliitolea tambiko miungu ya Damasko iliyokuwa imemshinda vitani akisema, “Maadamu miungu ya Shamu iliwasaidia wafalme wa Shamu, nikiitolea tambiko huenda ikanisaidia nami pia.” Lakini hiyo ilisababisha kuangamia kwake na taifa lote la Israeli. Zaidi ya hayo, alivikusanya vifaa vyote vya nyumba ya Mungu, akavikatakata vipandevipande, kisha akaifunga milango ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kujijengea madhabahu katika kila pembe ya Yerusalemu. Na katika kila mji wa Yuda, alitengeneza mahali pa kufukizia ubani miungu mingine. Kwa kutenda hivyo, alimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake. Matendo yake mengine na mienendo yake yote, kutoka mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Yuda na Israeli. Mfalme Ahazi alifariki, akazikwa mjini Yerusalemu, lakini si katika makaburi ya wafalme wa Israeli. Naye Hezekia mwanawe, akatawala mahali pake. Hezekia alianza kutawala Yuda akiwa na umri wa miaka ishirini na mitano, akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na tisa. Mama yake alikuwa Abiya binti Zekaria. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama vile alivyofanya Daudi, babu yake. Mnamo mwezi wa kwanza wa mwaka wa kwanza wa utawala wake, mfalme Hezekia aliifungua tena milango ya hekalu, akaitengeneza. Aliwaingiza makuhani na Walawi, kisha akawakusanya uani upande wa mashariki, akawaambia, “Nisikieni enyi Walawi! Jitakaseni na itakaseni nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu. Toeni uchafu wote uliomo patakatifu. Kwa maana babu zetu waliasi na kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Wamemwacha, wakageuzia mbali nyuso zao na kupawekea kisogo mahali aishipo Mwenyezi-Mungu. Tena, waliifunga milango ya ukumbi, wakazizima taa, na hawajafukiza ubani wala kutoa tambiko za kuteketeza katika mahali patakatifu pa Mungu wa Israeli. Kwa sababu hii, Mwenyezi-Mungu aliikasirikia sana Yuda na Yerusalemu, na yale aliyowatenda yamewashangaza na kuwaogofya watu wote, wakawazomea. Haya yote mmeyaona wenyewe kwa macho yenu. Baba zetu waliuawa vitani, na wana wetu na binti zetu na wake zetu ni mateka kwa sababu hiihii. Sasa, nimeamua kwa dhati kufanya agano na Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ili asitukasirikie zaidi. Basi wanangu, muwe na nidhamu. Mwenyezi-Mungu amewachagua nyinyi ili mumtumikie, muwaongoze watu wake katika ibada, na kumfukizia ubani.” Walawi wafuatao wakaanza kazi: Kutoka ukoo wa Kohathi walikuwa Mahathi mwana wa Amasai na Yoeli mwana wa Azaria; ukoo wa Merari: Kishi mwana wa Abdi na Azaria mwana wa Yehaleli; ukoo wa Gershoni: Yoa mwana wa Zima, na Edeni mwana wa Yoa; ukoo wa Elisafani: Shimori na Yeneli, ukoo wa Hemani: Zekaria na Matania; ukoo wa Yeduthuni: Shemaya na Uzieli. Hawa waliwakusanya Walawi wenzao, wakajitakasa. Kisha wakaingia kama walivyotakiwa kufanya na mfalme, wakaanza kusafisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu kama Mwenyezi-Mungu alivyoagiza. Makuhani waliingia katika sehemu ya ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakautoa uchafu wote uliokuwemo, wakauweka uani. Kutoka hapo, Walawi waliuchukua uchafu huo mpaka nje kwenye Bonde la Kidroni. Walianza kazi ya kulitakasa hekalu siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, na kufikia siku ya nane, wakawa wamekwisha maliza kazi yote, hata na ukumbini. Kisha, walifanya kazi kwa muda wa siku nane zaidi hadi siku ya kumi na sita ya mwezi huo, kila kitu kilikamilika. Baadaye, Walawi walimwendea mfalme Hezekia wakamwambia, “Tumekwisha litakasa hekalu lote pamoja na madhabahu ya tambiko za kuteketeza na vyombo vyake vyote, na meza ya mikate mitakatifu na vyombo vyake vyote. Tena, vyombo vyote ambavyo mfalme Ahazi alivyoviondoa wakati wa utawala wake, hapo alipoasi, tumevirudisha na kuviweka wakfu. Vyote vipo mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu.” Mapema kesho yake, mfalme Hezekia aliwakusanya wakuu wa mji, akaenda nao katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Wakaleta mafahali saba, kondoo madume saba, wanakondoo saba na mbuzi madume saba, wawe sadaka ya kuondoa dhambi, kwa ajili ya jamaa ya kifalme, patakatifu na watu wa Yuda. Hapo, mfalme aliwaambia makuhani waliokuwa wazawa wa Aroni wawateketeze juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu. Makuhani walichinja mafahali kwanza, kisha kondoo madume, halafu wanakondoo na kila mara walichukua damu ya wanyama hao na kunyunyiza juu ya madhabahu. Hatimaye, waliwaleta wale mbuzi madume wa sadaka ya kuondoa dhambi karibu na mfalme na watu wote waliokuwamo, nao wakaweka mikono yao juu ya hao mbuzi madume. Basi, wale makuhani wakawachinja, na kunyunyiza damu yao juu ya madhabahu ili iwe tambiko ya upatanisho kwa Waisraeli wote, kwa maana mfalme Hezekia alikuwa ameagiza itolewe sadaka ya kuteketeza na sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya Israeli yote. Mfalme Hezekia aliyafuata maagizo ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amempa mfalme Daudi kwa njia ya Gadi mwonaji wa mfalme na nabii Nathani. Hivyo basi, akaweka Walawi katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, baadhi yao wakiwa na matoazi, wengine vinanda na wengine vinubi. Hiyo ilikuwa amri ya Mwenyezi-Mungu kwa njia ya manabii wake. Walawi walisimama na vyombo vya muziki vya Daudi, pia makuhani walisimama wakiwa na tarumbeta zao. Basi, Hezekia akaamuru sadaka ya kuteketeza itolewe juu ya madhabahu. Mara tu tambiko hiyo ilipoanza kutolewa, watu walianza kumsifu Mwenyezi-Mungu kwa nyimbo zilizoandamana na mlio wa tarumbeta na vyombo vya muziki vya Daudi mfalme wa Israeli. Watu wote waliokuwamo walishiriki katika ibada. Waimbaji waliendelea kuimba, na tarumbeta zikaendelea kupigwa hadi shughuli za utoaji wa sadaka hiyo ya kuteketeza ilipokamilika. Hatimaye, mfalme Hezekia pamoja na watu wote waliokuwamo waliinama, wakamwabudu Mwenyezi-Mungu. Kisha mfalme Hezekia na viongozi wakawaambia Walawi wamsifu Mwenyezi-Mungu kwa nyimbo alizotunga mfalme Daudi na mwonaji Asafu. Basi, watu wote wakamtukuza Mungu kwa furaha, na kumsujudia. Ndipo Hezekia akawaambia watu, “Maadamu sasa mmekwisha jitakasa, karibieni, leteni sadaka na matoleo ya shukrani katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Basi, watu wakaleta sadaka zao na matoleo yao ya shukrani, na tambiko za kuteketeza. Sadaka za kuteketeza walizoleta jumla zilikuwa mafahali 70, kondoo madume 100 na wanakondoo 200. Zote hizo zilikuwa sadaka za kuteketeza kwa Mwenyezi-Mungu. Matoleo matakatifu yalikuwa mafahali 600 na kondoo 3,000. Kwa vile ambavyo idadi ya makuhani ilikuwa ndogo, hawakuweza kuwachuna wanyama hao wote. Kwa hiyo, ndugu zao Walawi waliwasaidia hadi walipokamilisha kazi hiyo. Wakati huo, makuhani wengine zaidi walikuwa wamekwisha jitakasa. (Walawi walijiweka katika hali ya usafi zaidi kuliko makuhani.) Mbali na wingi wa sadaka za kuteketeza, kulikuwako pia mafuta ya sadaka ya amani, hata kulikuwapo sadaka ya kinywaji kwa sadaka za kuteketeza. Hivyo basi, huduma za ibada zikaanzishwa tena hekaluni. Mfalme Hezekia na watu wote wakajawa na furaha tele kwa sababu ya yote Mungu aliyowatendea watu; maana tukio hili lilitokea ghafla. Mfalme Hezekia aliwatumia ujumbe watu wote wa Israeli na Yuda, na pia akawaandikia barua wenyeji wa Efraimu na Manase, akiwaalika wote waje katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu Yerusalemu, ili kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka kwa heshima yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Mfalme, viongozi na watu wote wa mji wa Yerusalemu waliafikiana kuiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka mnamo mwezi wa pili badala ya mwezi wa kwanza kama ilivyokuwa kawaida, kwa sababu idadi ya makuhani waliokuwa wamekwisha kujiweka wakfu ilikuwa ndogo, nao watu walikuwa bado hawajakusanyika Yerusalemu. Aidha, mpango huu ulimridhisha mfalme pamoja na watu wote waliokuwa wamekusanyika. Kwa hiyo waliamua kutoa tangazo kote nchini Israeli, kutoka Beer-sheba hadi Dani, kwamba watu waje Yerusalemu kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Ulikuwa umepita muda mrefu kabla watu hawajaiadhimisha Pasaka kulingana na sheria zake. Matarishi, kwa amri yake mfalme na maofisa wake, walipeleka barua kote nchini Israeli na Yuda. Barua hizo zilikuwa na ujumbe ufuatao: “Enyi watu wa Israeli mlionusurika baada ya mashambulizi ya wafalme wa Ashuru. Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, ili naye apate kuwarudieni. Msiwe kama babu zenu na ndugu zenu ambao hawakuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, ambaye kama mnavyoona aliwaadhibu vikali. Msiwe wakaidi kama babu zenu, ila mtiini Mwenyezi-Mungu. Njoni katika hekalu lake ambalo amelitakasa milele, mumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili asiwakasirikie. Mkimrudia Mwenyezi-Mungu, wale ambao waliwateka ndugu zenu na watoto wenu, watawahurumia na kuwaacha warudi katika nchi hii. Kwa maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni mwenye rehema na huruma, naye atawapokea ikiwa mtamrudia.” Basi, matarishi hao wakaenda toka mji mmoja hadi mwingine kote nchini Efraimu na Manase, wakafika hata Zebuluni. Lakini watu waliwacheka na kuwadhihaki. Hata hivyo, watu wachache miongoni mwa makabila ya Asheri, Manase na Zebuluni, walijinyenyekesha wakaja Yerusalemu. Nguvu ya Mungu ilikuwa ikifanya kazi katika Yuda, akawapa moyo kutii amri za mfalme na maofisa wake kadiri ya maagizo ya Mwenyezi-Mungu. Watu wengi sana walijumuika mjini Yerusalemu mnamo mwezi wa pili, kuiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu. Walianza kazi, wakaziondoa madhabahu zote zilizokuwa Yerusalemu, na nyingine zote zilizotumiwa kufukizia ubani, wakazibeba na kuzitupa katika Bonde la Kidroni. Siku ya kumi na nne ya mwezi huo walichinja mwanakondoo wa Pasaka. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketeza katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Walichukua nafasi zao hekaluni kulingana na maagizo yaliyokuwamo katika sheria za Mose, mtu wa Mungu. Walawi waliwapa makuhani damu ya tambiko, nao wakainyunyiza madhabahuni. Kwa vile wengi wa wale waliokusanyika hapo hawakuwa wamejitakasa, iliwabidi Walawi kuwachinjia wanakondoo wa Pasaka na kuwaweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Aidha miongoni mwa kusanyiko hilo la watu, wengi wa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zebuluni, walikuwa wakiiadhimisha Pasaka kinyume cha maagizo. Hii ni kwa kuwa mfalme Hezekia aliwaombea akisema, “Mwenyezi-Mungu uliye mwema, msamehe yeyote yule atakayekuomba kwa moyo wake wote wewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake, hata ingawa si msafi kulingana na sheria za utakaso.” Mwenyezi-Mungu alikubali ombi la Hezekia, akawasamehe watu hao. Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika mjini Yerusalemu waliiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu kwa muda wa siku saba, wakiwa na furaha kubwa. Walawi na makuhani walimsifu Mwenyezi-Mungu kila siku, walimwimbia kwa nguvu zao zote. Mfalme Hezekia aliwasifu na kuwatia moyo makuhani kwa kuwa waliendesha ibada kwa ujuzi mwingi. Baada ya kumaliza siku saba wakati ambao watu walikula, wakatoa sadaka za amani na kumtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, watu waliamua kwa kauli moja kuziendeleza sherehe kwa muda wa siku saba zaidi. Basi, wakaendelea kusherehekea kwa furaha kuu kwa muda wa siku saba zaidi. Mfalme Hezekia wa Yuda aliwapa watu waliokusanyika jumla ya mafahali 1,000 na kondoo 7,000. Hali kadhalika, wakuu wakawapa mafahali 1,000 na kondoo 10,000. Idadi kubwa ya makuhani walijitakasa. Kila mtu aliyehudhuria alifurahi sana. Watu wote wa Yuda, makuhani na Walawi, wakazi wa Yerusalemu waliohudhuria, wageni waliotoka nje ya Yerusalemu na wale walioishi Yuda, wote walifurahi sana. Kukawa na furaha kuu mno Yerusalemu, maana tangu enzi ya mfalme Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli, jambo kama hilo lilikuwa halijatokea Yerusalemu. Kisha, makuhani na Walawi wakawaombea watu baraka zake Mwenyezi-Mungu, naye katika makao yake matakatifu huko mbinguni akayasikia maombi yao na kuyakubali. Baada ya sherehe kumalizika, watu wote wa Israeli walikwenda katika kila mji wa Yuda, wakavunjavunja nguzo za mawe na kuzikatakata sanamu za Ashera, mungu wa kike, na pia wakaziharibu madhabahu na mahali pa kuabudia miungu mingine. Walifanya vivyo hivyo kote katika Yuda, Benyamini, Efraimu na Manase, mpaka walipokwisha kuharibu vyote. Kisha wakarudi mjini mwao, kila mtu kwenye milki yake. Mfalme Hezekia aliwapanga tena makuhani na Walawi katika makundi, akampa kila mmoja wao wajibu maalumu, kuhudumu katika sehemu mbalimbali za hekalu la Mwenyezi-Mungu. Wajibu huo ni pamoja na utoaji wa sadaka za kuteketeza na za amani, kushukuru na kusifu. Kutokana na mali yake mwenyewe, mfalme alitoa sehemu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa asubuhi na jioni, sadaka za siku ya Sabato na wakati wa sherehe za kuadhimisha mwezi mwandamo na zile sikukuu nyingine zilizoamriwa kulingana na sheria ya Mwenyezi-Mungu. Zaidi ya hayo, mfalme aliwaambia wenyeji wa Yerusalemu watoe sehemu waliyostahili kupewa makuhani na Walawi, ili wao wajitolee kikamilifu katika shughuli za sheria za Mwenyezi-Mungu. Mara tu amri hii ilipotolewa, watu wa Israeli walitoa kwa wingi, malimbuko ya nafaka, divai, mafuta, asali na mazao mengine mbalimbali ya shambani, na pia zaka nyingi za kila kitu. Watu wa Israeli na Yuda walioishi katika miji ya Yuda, pia wakaleta zaka zao za ng'ombe na kondoo na vitu vingine, wakaviweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Waliviweka vitu hivyo katika mafungu. Katika mwezi wa tatu walianza kuvipanga katika mafungu, wakamaliza mnamo mwezi wa saba. Mfalme Hezekia na maofisa wake walipokuja kuyaona mafungu hayo, walimtukuza Mwenyezi-Mungu na watu wake wa Israeli. Mfalme Hezekia aliwauliza makuhani na Walawi kuhusu mafungu hayo. Azaria, kuhani mkuu aliyekuwa wa uzao wa Sadoki akamjibu, “Tangu watu waanze kuleta matoleo yao hekaluni, tumekuwa na vyakula vya kutosha na hata tunayo akiba kubwa. Mwenyezi-Mungu amewabariki watu wake, ndiyo maana tumepata vitu hivi vyote.” Kisha mfalme Hezekia akawaamuru watengeneze ghala katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Wakatengeneza; na humo wakaweka matoleo, zaka na vyote vilivyowekwa wakfu, kwa uaminifu. Wakamweka Konania, Mlawi, awe ofisa mkuu mtunzaji wa vitu hivyo, na Shimei nduguye, awe msaidizi wake. Nao Yehieli, Azazia, Nahathi, Asaheli, Yeremothi, Yozabadi, Elieli, Ismakia, Mahathi na Benaya, waliwekwa wawe wasimamizi chini ya uongozi wa Konania na Shimei nduguye. Hawa wote walichaguliwa na mfalme Hezekia na Azaria, ofisa mkuu wa nyumba ya Mungu. Kore mwana wa Imna, Mlawi, aliyekuwa bawabu wa Lango la Mashariki la hekalu, alisimamia matoleo yote ya hiari kwa Mungu, na ugawaji wa matoleo kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na sadaka zilizo takatifu kabisa. Nao Edeni, Miniamini, Yeshua, Shemaya, Amaria na Shekania, walimsaidia kufanya kazi hiyo kwa uaminifu katika ile miji mingine walimoishi makuhani. Waliwagawia ndugu zao Walawi vyakula, wakubwa kwa wadogo. Tena, bila kujali koo walimoandikishwa, waliwapa sehemu wale watoto wa kiume waliokuwa wametimiza umri wa miaka mitatu na zaidi, na ambao waliingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kila siku kutekeleza wajibu wao. Kila mmoja wao alipata sehemu yake kulingana na huduma aliyotoa kwa zamu yake. Makuhani waliandikishwa kulingana na jamaa zao, hali Walawi waliotimiza miaka ishirini na zaidi waliandikishwa kulingana na kazi zao na zamu zao. Waliandikishwa wote pamoja na watoto wao wadogo, wake zao, wana wao na binti zao kwa kuwa, kwa mujibu wa kazi zao, walihitajika kujiweka katika hali ya utakaso kila mara. Vilevile, miongoni mwa wazawa wa Aroni, makuhani waliokuwa wanakaa katika mashamba waliyomiliki kwa pamoja nje ya miji yao, mlikuwa watu maalumu kwenye miji hiyo ambao waliwagawia sehemu zao za vyakula. Waliwapa sehemu kila mwanamume katika jamaa za makuhani, na kila mmoja aliyekuwa ameandikishwa kati ya Walawi. Hivyo ndivyo mfalme Hezekia alivyotenda yaliyo mema, ya haki na ya uaminifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kote nchini Yuda. Kila kazi aliyoifanya katika utumishi wa nyumba ya Mungu au katika utekelezaji wa sheria na amri za Mungu ili kufuata uongozi kutoka kwake, alizifanya kwa moyo wake wote, naye akafanikiwa. Baada ya mambo yote hayo ya uaminifu ya mfalme Hezekia, mfalme Senakeribu wa Ashuru aliivamia Yuda. Alikuja akapiga makambi kwenye miji yenye ngome akitumaini kwamba ataishinda iwe mali yake. Mfalme Hezekia alipoona kwamba mfalme Senakeribu amekuja kwa kusudi la kuishambulia Yerusalemu, aliamua, yeye pamoja na maofisa wake wakuu wa majeshi kuyafunga maji ya chemchemi zilizokuwa nje ya miji; nao wakamuunga mkono, wakamsaidia. Wakawakusanya watu wengi pamoja wakazifunga chemchemi zote pamoja na kijito kilichopitia kati ya sehemu hiyo wakisema, “Ya nini kuwaachia wafalme wa Ashuru wakija wakute maji tele?” Ili kuuhami mji, mfalme Hezekia alipiga moyo konde, akajenga upya ukuta wote uliokuwa umebomoka, na juu yake akajenga minara. Upande wa nje, akajenga ukuta mwingine wa pili, na akaiimarisha sehemu iliyoitwa Milo katika mji wa Daudi. Zaidi ya hayo alitengeneza silaha na ngao kwa wingi. Aliwaweka watu wote mjini chini ya makamanda, kisha akawaamuru wakusanyike uwanjani penye Lango la Mji. Hapo akawatia moyo akisema, “Muwe imara na hodari. Msiogope wala msifadhaike mbele ya mfalme wa Ashuru au majeshi yake maana tuliye naye ni mkuu kuliko aliye naye Senakeribu. Yeye anazo nguvu za kibinadamu tu, hali sisi tunaye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Maneno haya ya mfalme Hezekia yaliwatia moyo sana watu hao. Baada ya hayo, Senakeribu mfalme wa Ashuru, ambaye bado alikuwa ameuzingira mji wa Lakishi akiwa na majeshi yake yote, aliwatuma watumishi wake Yerusalemu kwa Hezekia mfalme wa Yuda na kwa watu wote wa Yuda waliokuwa Yerusalemu, akisema “Hivi ndivyo anavyosema Senakeribu mfalme wa Ashuru: Je, mnategemea nini hata mnakaa Yerusalemu, mji ambao umezingirwa? Je, si kana kwamba Hezekia anawadanganya ili awafanye mfe kwa njaa au kiu anapowaambia, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawaokoa mikononi mwa mfalme wa Ashuru?’ Je, siye huyu Hezekia aliyepaharibu mahali pake pa kuabudia na madhabahu zake na kuwaamuru watu wote wa Yuda na Yerusalemu akisema: ‘Mtaabudu mbele ya madhabahu moja, na juu yake mtateketeza sadaka zenu?’ Je, kwani hamjui yale yote ambayo mimi na babu zangu tumewatenda watu wote wa mataifa mengine? Je, miungu ya mataifa ya nchi hizo iliweza kuzikomboa nchi zao mkononi mwangu? Ni mungu gani kati ya miungu ya mataifa hayo iliyoharibiwa kabisa na babu zangu aliyeweza kuwakomboa watu wake kutoka mikononi mwangu ndio nanyi muwe na tumaini ya kwamba Mungu wenu atawaokoeni mikononi mwangu? Msidanganywe na Hezekia wala msishawishike kwa hayo. Msimwamini mtu huyu, kwa maana hapajatokea mungu wa taifa au mfalme yeyote aliyefaulu kuwakomboa watu wake kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru, sembuse huyu Mungu wenu!” Watumishi wa mfalme wa Ashuru walisema maneno mengine mengi mabaya dhidi ya Mwenyezi-Mungu, na dhidi ya Hezekia mtumishi wake. Mfalme mwenyewe aliandika barua akamtukana na kumdharau Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akisema, “Kama vile ambavyo miungu ya mataifa mengine haikuweza kuwaokoa watu wao kutoka mikononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake.” Maofisa hao waliwaambia kwa sauti kubwa kwa lugha ya Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa ukutani, wakikusudia kuwatia hofu na woga ili wauteke mji kwa urahisi. Wakazungumza juu ya Mungu wa Yerusalemu kana kwamba ni miungu ya mataifa mengine; sanamu tu zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu! Hapo mfalme Hezekia na nabii Isaya, mwana wa Amozi, wakamwomba Mungu na kumlilia awasaidie kwa ajili ya mambo haya. Naye Mwenyezi-Mungu akatuma malaika, akaenda na kuwakatilia mbali mashujaa, wanajeshi, makamanda na maofisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Basi, mfalme wa Ashuru akarejea nchini mwake amejawa aibu. Mara alipoingia ndani ya nyumba ya mungu wake, baadhi ya wanawe mwenyewe wakamuua papo hapo kwa upanga. Kwa njia hii basi, Mwenyezi-Mungu akamwokoa mfalme Hezekia na wakazi wa Yerusalemu kutoka mkono wa Senakeribu mfalme wa Ashuru, na kutoka mkono wa maadui wake wote. Akawapa maisha ya amani na jirani zake wote. Watu wengi sana walikuja wakamletea Mwenyezi-Mungu tambiko huko Yerusalemu, pia wakamletea Hezekia, mfalme wa Yuda zawadi za thamani. Hivyo kutoka wakati huo, akasifiwa sana na mataifa mengine yote. Wakati huo, Hezekia aliugua sana, karibu na kufa. Akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akamjibu na kumpa ishara. Lakini Hezekia hakumtolea Mwenyezi-Mungu shukrani kwa hayo yote aliyomtendea kwa kuwa moyo wake ulikuwa umejaa majivuno. Hii ilisababisha kutaabika kwa Yuda na Yerusalemu. Kwa hiyo ghadhabu ikawa juu yake, juu ya Yuda na juu ya Yerusalemu. Hatimaye Hezekia alinyenyekea akaacha kuwa na moyo uliojaa majivuno; yeye na wakazi wa Yerusalemu walijinyenyekesha kwa hiyo ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu haikuwajia wakati Hezekia alipokuwa hai. Mfalme Hezekia alitajirika sana, akaheshimiwa. Alijitengenezea hazina za fedha, za dhahabu, za vito, za viungo, ngao na za aina zote za vyombo vya thamani kubwa. Aidha, alijijengea mabohari ya kuhifadhia mazao ya nafaka, divai na mafuta, na mazizi kwa ajili ya ng'ombe na mengine kwa ajili ya kondoo. Vivyo hivyo alijiongezea miji kwa ajili yake mwenyewe, makundi mengi ya ng'ombe na kondoo kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimkirimia mali nyingi. Mfalme Hezekia ndiye aliyeyafunga maji ya chemchemi ya Gihoni, akayachimbia mfereji wa chini kwa chini hadi upande wa magharibi wa mji wa Daudi. Hezekia alifaulu katika kila jambo alilofanya, na hata wakati ambapo mabalozi wa wakuu wa Babuloni waliotumwa kwake kuuliza juu ya mambo ya ajabu yaliyotokea humo, Mungu, alimwacha ajiamulie mwenyewe, ili amjaribu na kujua yote yaliyokuwa moyoni mwake. Matendo mengine ya mfalme Hezekia na wema wake, yameandikwa katika Maono ya nabii Isaya mwana wa Amozi, katika Kitabu cha Wafalme wa Yuda na Israeli. Hezekia alifariki dunia na kuzikwa kwenye sehemu ya juu ya makaburi ya wafalme. Watu wote wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu walimtolea heshima kuu wakati wa kifo chake, naye Manase, mwanawe, akatawala mahali pake. Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala, akatawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa miaka hamsini na mitano. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kuiga mienendo miovu ya mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafukuza wakati watu wake wa Israeli walipokuwa wanaingia nchini. Kwa maana alirekebisha mahali pa kuabudia miungu mingine palipokuwa pamebomolewa na Hezekia baba yake; akajenga madhabahu za kuabudia Mabaali, akatengeneza na sanamu za Maashera. Isitoshe, aliabudu vitu vyote vya mbinguni na kuvitumikia. Alijenga madhabahu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema, “Jina langu litaabudiwa milele katika Yerusalemu.” Alijenga madhabahu za kuabudia vitu vyote mbinguni kwenye nyua mbili za nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Pia aliwatoa wanawe kama sadaka ya kuteketeza katika bonde la mwana wa Hinomu. Alipiga ramli, alibashiri na alitumia hirizi; hata alishirikiana na waaguzi wa mizimu na wachawi. Alitenda maovu mengi mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamkasirisha. Nayo sanamu aliyoitengeneza, aliiweka katika nyumba ya Mungu mahali alipopazungumzia, mbele ya Daudi na Solomoni mwanawe: “Katika nyumba hii na katika Yerusalemu kati ya makabila kumi na mawili ya Israeli, ndipo mahali nitakapoabudiwa milele. Na iwapo watu wa Israeli watajali kutenda yote niliyowaamuru, wakatii sheria zote, masharti, na maagizo yaliyotolewa kwa mkono wa Mose, basi kamwe sitawaacha wafukuzwe kutoka katika nchi hii ambayo niliwapa babu zao.” Lakini Manase aliwapotosha watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, wakatenda maovu zaidi kuliko mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyaangamiza mbele ya watu wa Israeli. Mwenyezi-Mungu alimwonya Manase na watu wake, lakini hawakumsikia. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu akawaleta makamanda wa jeshi la mfalme wa Ashuru. Hao makamanda walimkamata Manase kwa kulabu wakamfunga pingu za shaba, wakampeleka hadi Babuloni. Wakati alipokuwa taabuni, alimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akajinyenyekesha sana mbele ya Mungu wa babu zake. Alimsihi, naye Mungu akapokea ombi lake na sala yake akamrudisha Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu. Baada ya haya, Manase alijenga ukuta mwingine upande wa nje wa mji wa Daudi, magharibi mwa Gihoni, bondeni, akauendeleza hadi Lango la Samaki, akauzungusha hadi Ofeli; akauinua juu sana. Pamoja na hayo, aliweka makamanda wa majeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome. Alitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu miungu yote ya kigeni na sanamu pamoja na madhabahu zote alizokuwa amezijenga kwenye mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika Yerusalemu; alivitupa nje ya mji. Alirudisha madhabahu ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, na juu yake akatoa tambiko za amani na za shukrani, akawaamuru watu wa Yuda wamwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Hata hivyo watu waliendelea kutoa sadaka mahali pa kufanyia ibada, lakini kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao tu. Matendo mengine ya Manase, sala yake kwa Mungu wake na maneno ya waonaji waliozungumza naye kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hayo, yote yameandikwa katika Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Nalo ombi lake na jinsi Mungu alivyompokea, dhambi zake zote na ukosefu wa uaminifu wake, mahali alipojenga pa kuabudia na jinsi alivyotengeneza Ashera na sanamu kabla ya kujinyenyekesha, hayo yameandikwa katika Kumbukumbu za Waonaji. Manase alifariki na kuzikwa katika ikulu yake, naye Amoni, mwanawe, akatawala mahali pake. Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala Yuda; alitawala miaka miwili huko Yerusalemu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama vile Manase baba yake alivyofanya. Pia alitoa sadaka na kutumikia sanamu ambazo Manase baba yake alichonga. Naye hakujinyenyekesha mbele za Mwenyezi-Mungu, kama alivyofanya Manase, lakini yeye aliongeza kutenda makosa zaidi. Baadaye watumishi wake walikula njama na kumuua katika ikulu yake. Lakini watu wa Yuda wakawaua hao wote waliokula njama dhidi ya Amoni; kisha wakamfanya Yosia, mwanawe kuwa mfalme badala yake. Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; alitawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu. Alifuata njia zake Daudi babu yake, na kushika amri za Mwenyezi-Mungu kwa dhati. Katika mwaka wa nne wa utawala wake, mfalme Yosia, akiwa bado kijana, alianza kumwabudu Mungu wa Daudi, baba yake. Baadaye alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili alianza kuisafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuharibu mahali pa kuabudia miungu mingine, sanamu za Ashera, na sanamu nyinginezo za kuchonga na za kusubu. Watu wake walizibomoa madhabahu za ibada za Mabaali mbele yake na alizikatakata madhabahu za kufukizia ubani zilizoinuliwa juu ya madhabahu hizo; pia alizipondaponda sanamu za Ashera na nyinginezo za kuchonga na za kusubu; alizifanya kuwa mavumbi, nayo mavumbi akayamwaga juu ya makaburi ya wale ambao hapo awali walizitolea sadaka. Aidha, aliiteketeza mifupa ya makuhani wa miungu hiyo kwenye madhabahu zao, hivyo akatakasa Yuda na Yerusalemu. Alifanya vivyo hivyo katika miji ya Manase, Efraimu, Simeoni mpaka Naftali na kwenye magofu yaliyokuwa kandokando ya miji hiyo. Alizibomoa madhabahu na kupondaponda Maashera na sanamu za kuchongwa zikawa mavumbi. Kadhalika alizikatakata madhabahu za kufukizia ubani katika nchi yote ya Israeli. Hatimaye alirudi Yerusalemu. Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, wakati ambapo alikuwa amekwisha takasa nchi na nyumba, alituma watu watatu: Shafani mwana wa Azalia, Maaseya gavana wa mji na Yoa mwana wa Yoahazi, Katibu, ili waende kuirekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. Walimwendea Hilkia, kuhani mkuu, wakamkabidhi fedha zilizokuwa zimeletwa katika nyumba ya Mungu ambazo zilikusanywa na Walawi wangojamlango, kutoka Manase, Efraimu na kutoka pande nyingine zote za Israeli, nchi yote ya Yuda na Benyamini, na pia kutoka kwa wenyeji wa Yerusalemu. Zilikabidhiwa wale mafundi waliosimamia marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu; na mafundi waliofanya kazi katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu walizitoa ili kutengeneza na kurekebisha nyumba. Waliwapatia maseremala na wajenzi kwa ajili ya kununulia mawe yaliyochongwa, mbao za kuunganishia na mihimili ya kutumia katika kurekebisha yale majengo ambayo wafalme wa Yuda waliyaacha yakabomokabomoka. Watu hao waliifanya kazi hiyo kwa uaminifu, wakiwa chini ya uongozi wa Walawi Yahathi na Obadia, chini ya wana wa Merari na Zekaria na Meshulamu na chini ya wazawa wa Kohathi. Walawi wote waliokuwa na ujuzi sana katika upigaji wa vyombo vya muziki, waliwasimamia wachukuzi wa mizigo na kuwaongoza wote waliofanya kazi mbalimbali; baadhi ya Walawi walikuwa waandishi, maofisa na hata walinda mlango. Wakati walipokuwa wanashughulika na utoaji wa fedha zilizokuwa zimeletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kuhani Hilkia alipata Kitabu cha Sheria ya Mwenyezi-Mungu iliyotolewa kwa mkono wa Mose. Kisha Hilkia alimwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Sheria katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Halafu Hilkia akampatia Shafani kitabu. Naye Shafani akampelekea mfalme na kumpasha habari, akisema, “Yote watumishi wako waliyokabidhiwa wanayafanya. Wametoa fedha zilizopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, halafu wamezikabidhi kwa wasimamizi na mafundi.” Kisha Katibu Shafani akamwambia mfalme, “Kuhani Hilkia amenipa kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme. Mfalme aliposikia maneno ya sheria alirarua mavazi yake. Ndipo alipomwamuru Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani, Abdoni mwana wa Mika, katibu Shafani na Asaya, mtumishi wa mfalme, akisema, “Nendeni mkatafute shauri kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwa niaba yangu na watu ambao wamebaki katika Israeli na Yuda, kuhusu maneno yaliyomo katika kitabu kilichopatikana. Kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imetuangukia, maana babu zetu hawakushika neno la Mwenyezi-Mungu, wala kufanya yaliyoandikwa humo.” Kwa hiyo Hilkia pamoja na wale wengine mfalme aliowatuma walimwendea nabii Hulda, mkewe Shalumu, mwana wa Tokathi, mwana wa Hasra, mtunza mavazi yaliyotumika hekaluni (alikuwa anaishi Yerusalemu katika mtaa wa pili); nao walizungumza naye juu ya mambo yaliyotokea. Basi akawaambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambie huyo aliyewatuma kwangu, Mwenyezi-Mungu anasema hivi, ‘Tazama nitaleta uovu juu ya Yerusalemu na juu ya wakazi wake, laana zote zilizoandikwa katika kitabu kilichosomwa mbele ya mfalme wa Yuda. Kwa sababu wameniacha mimi na kufukizia miungu mingine ubani ili wanikasirishe sana kwa kazi zote za mikono yao, basi ghadhabu yangu itamwagika juu ya mahali hapa wala haitatulizwa. Lakini kumhusu mfalme wa Yuda, aliyewatuma kutafuta shauri la Mwenyezi-Mungu mwambie kwamba, hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli juu ya maneno uliyoyasikia: Kwa kuwa umetubu na kunyenyekea mbele yangu, hata umerarua mavazi yako na kulia uliposikia maneno yangu dhidi ya mahali hapa, na dhidi ya wakazi wake, na umejinyenyekesha mbele yangu, nami pia nimekusikia. Adhabu ambayo nitailetea Yerusalemu, sitaileta wakati wa uhai wako. Utawala wako utakuwa wa amani.’” Basi, wajumbe wakamletea mfalme Yosia habari hizi. Kisha mfalme Yosia aliita na kukusanya viongozi wote wa Yuda na Yerusalemu. Naye mfalme akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu pamoja na wanaume wote wa Yuda, na wakazi wa Yerusalemu wakifuatana na makuhani, Walawi na watu wengine wote wakubwa kwa wadogo. Ndipo alipowasomea maneno ya kitabu cha agano kilichopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu mfalme alisimama mahali pake akafanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu, kumfuata Mwenyezi-Mungu, kushika amri, maamuzi na masharti yake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, kutenda maneno yote ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hicho. Tena aliwafanya wote waliokuwa katika Yerusalemu na katika Benyamini kuzingatia agano. Nao wakazi wa Yerusalemu waliishi kwa kufuata agano la Mungu, Mungu wa babu zao. Kisha Yosia aliondoa sanamu zote za kuchukiza zilizokuwa katika eneo lote la watu wa Israeli, na kuwahimiza watu wote wa Israeli kumtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Katika maisha yake yote hawakumwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. Mfalme Yosia aliadhimisha Pasaka mjini Yerusalemu, wakachinja wanakondoo wa Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Aliwateua makuhani kwa kazi zao ambazo walihitajika kufanya katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuwatia moyo wazifanye kikamilifu. Pamoja na hayo, aliwapa Walawi waliowafundisha watu wa Israeli na ambao walikuwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, maagizo yafuatayo: “Liwekeni sanduku takatifu ndani ya nyumba ambayo Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli alijenga; hamhitaji kulibebabeba tena mabegani. Sasa mtumikieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu na watu wake Waisraeli. Timizeni wajibu wenu kulingana na koo zenu, kufuatana na maagizo ya Daudi mfalme wa Israeli na Solomoni mwanawe. Simameni pia mahali patakatifu kama wawakilishi wa jamaa za koo zenu wasiofanya kazi za ukuhani, na kila mmoja aiwakilishe jamaa moja ya Walawi. Mchinjeni mwanakondoo wa Pasaka, mjitakase, halafu itayarisheni kwa ajili ya ndugu zenu, ili waweze kutimiza agizo la Mwenyezi-Mungu lililosemwa na Mose.” Kisha Yosia aliwapa watu, wanambuzi wapatao 30,000, na mafahali 3,000, wote hawa walitolewa kwenye mifugo ya mfalme. Nao maofisa wake, kwa hiari yao, walitoa mchango wao wakawapa watu, makuhani na Walawi. Hilkia, Zekaria na Yehieli, maofisa wa nyumba ya Mungu, waliwapa makuhani wanakondoo na wanambuzi 2,600 na mafahali 300 kwa ajili ya sadaka za Pasaka. Naye Konania na nduguze wawili, Shemaya na Nethaneli, pamoja na Hashabia, Yeieli na Yozabadi, waliokuwa viongozi wa Walawi, nao pia waliwapa wanakondoo na wanambuzi 5,000 na mafahali 500, kwa ajili ya sadaka za Pasaka. Baada ya matayarisho yote ya Pasaka kumalizika, makuhani walisimama mahali pao, na Walawi katika makundi yao; sawasawa na amri ya mfalme. Walimchinja mwanakondoo wa Pasaka, nao makuhani walinyunyiza damu, waliyopokea kutoka kwao nao Walawi waliwachuna wanyama. Halafu walitenga sadaka za kuteketeza ili waweze kuzigawa kulingana na jamaa zao walio makuhani ili wamtolee Mwenyezi-Mungu kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Mose. Nayo mafahali waliwafanya vivyo hivyo. Walimchoma mwanakondoo wa Pasaka juu ya moto kama ilivyoagizwa, na pia walizitokosa sadaka takatifu katika vyungu, masufuria na kwenye vikaango, na kuwagawia upesiupesi watu wasiofanya kazi ya ukuhani. Baadaye, Walawi wakajiandalia sehemu zao na za makuhani kwa maana makuhani wa uzao wa Aroni walikuwa wanashughulika na utoaji wa sadaka za kuteketeza, na vipande vya mafuta, mpaka usiku; kwa hiyo Walawi waliandaa kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani wa uzao wa Aroni. Nao waimbaji wazawa wa Asafu walishika nafasi zao, kwa mujibu wa maagizo ya mfalme Daudi, Asafu, Hemani na Yeduthuni, mwonaji wa mfalme. Nao mabawabu walikuwa kwenye malango; hawakuhitajika kuziacha nafasi zao za kazi kwa kuwa ndugu zao Walawi waliwaandalia Pasaka. Hivyo basi, huduma yote ya Mwenyezi-Mungu ilitayarishwa siku hiyo, ili kuiadhimisha Pasaka na kutoa sadaka za kuteketeza kwenye madhabahu ya Mwenyezi-Mungu kama alivyoamuru mfalme Yosia. Wakati huo watu wote wa Israeli waliohudhuria waliiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka na sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, kwa muda wa siku saba. Pasaka kama hiyo ilikuwa haijasherehekewa katika Israeli yote tangu siku za nabii Samueli. Hapajatokea mfalme hata mmoja wa Israeli aliyeadhimisha Pasaka kama hii iliyoadhimishwa na mfalme Yosia pamoja na makuhani, Walawi na watu wote wa Yuda, watu wa Israeli na wakazi wa Yerusalemu. Pasaka hiyo iliadhimishwa katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake mfalme Yosia. Baada ya haya yote aliyofanya mfalme Yosia kwa ajili ya hekalu, Neko, mfalme wa Misri, aliongoza jeshi lake kwenda kushambulia Karkemishi kwenye mto Eufrate. Naye mfalme Yosia alitoka kumkabili, lakini mfalme Neko akamtumia ujumbe usemao: “Vita hivi havikuhusu wewe hata kidogo ewe mfalme wa Yuda. Sikuja kupigana nawe bali dhidi ya maadui zangu, na Mungu ameniamuru niharakishe. Acha basi kumpinga Mungu, ambaye yu upande wangu, la sivyo atakuangamiza.” Lakini Yosia hakukubali kumwachia. Alikataa kuyasikiliza maneno aliyonena Mungu kwa njia ya Neko, kwa hiyo akajibadilisha ili asitambulike, kisha akaingia vitani katika tambarare ya Megido. Nao wapiga upinde walimpiga mshale mfalme Yosia; basi ndipo mfalme alipowaambia watumishi wake: “Niondoeni! Nimejeruhiwa vibaya sana.” Watumishi wake walimtoa katika gari lake la farasi, wakambeba na gari lake la pili hadi Yerusalemu. Hapo akafariki dunia na kuzikwa katika makaburi ya kifalme. Watu wote wa Yuda na Yerusalemu waliomboleza kifo cha Yosia. Nabii Yeremia pia alitunga shairi la maombolezo kwa ajili ya kifo chake; nao waimbaji wote, wanaume kwa wanawake, humtaja Yosia katika maombolezo yao, mpaka leo. Imekuwa desturi kufanya maombolezo haya katika Israeli. Hayo yameandikwa katika Maombolezo. Matendo mengine ya Yosia na matendo yake mema kama yalivyoandikwa katika sheria ya Mwenyezi-Mungu, na matendo yake tangu mwanzo hadi mwisho, hayo yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Israeli na Yuda. Watu wa Yuda walimtwaa Yehoahazi, mwana wa Yosia, wakamtawaza awe mfalme mahali pa baba yake. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala kwa muda wa miezi mitatu huko Yerusalemu. Baadaye mfalme wa Misri alimwondoa huko Yerusalemu na akaitoza nchi kodi ya kilo 3,400 za fedha na kilo 34 za dhahabu. Kisha mfalme wa Misri akamweka Eliakimu, nduguye Yehoahazi, kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu, akabadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu; lakini Neko akamtwaa Yehoahazi nduguye mpaka Misri. Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, akatawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. Nebukadneza mfalme wa Babuloni, alimshambulia, akamfunga kwa pingu ili kumpeleka mateka Babuloni. Nebukadneza pia alitwaa baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu akavipeleka Babuloni na kuviweka katika ikulu yake huko Babuloni. Basi, matendo mengine ya Yehoyakimu, pamoja na machukizo aliyotenda na mengine yaliyoonekana dhidi yake tazama yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Israeli na Yuda. Yehoyakini mwanawe alitawala badala yake. Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala. Alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miezi mitatu na siku kumi. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mwaka ulipokwisha, mfalme Nebukadneza alituma wajumbe, wakamchukua Yehoyakini mateka hadi Babuloni, pamoja na vyombo vya thamani vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Akamtawaza Sedekia, nduguye, kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka kumi na mmoja. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, wala hakunyenyekea mbele ya nabii Yeremia ambaye alisema maneno yaliyotoka kwa Mwenyezi-Mungu. Sedekia alimwasi pia mfalme Nebukadneza aliyekuwa amemfanya aape kwa jina la Mungu kwamba hatamwasi. Alikuwa mkaidi sana na mwenye kiburi akakataa kumgeukia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Hata makuhani, viongozi wa Yuda pamoja na watu walikosa uaminifu kabisa wakiiga matendo yote ya kuchukiza ya watu wa mataifa mengine; waliichafua nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambayo yeye mwenyewe alikuwa ameitakasa huko Yerusalemu. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, mara kwa mara alituma kwao wajumbe wake maana alikuwa na huruma kwa watu wake na makao yake. Lakini wao waliendelea kuwadhihaki wajumbe wa Mungu, wakayapuuza maneno yake na kuwacheka manabii wake mpaka hatimaye ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya watu wake hata kusiwe na namna yoyote ya kutoroka. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu alimleta mfalme wa Wakaldayo ambaye aliwaangamiza vijana wao kwa upanga hata ndani ya mahali patakatifu; wala hakumhurumia mtu yeyote awe mvulana au msichana, mzee au mnyonge. Wote Mwenyezi-Mungu aliwatia mikononi mwake. Alitwaa vyombo vyote vya nyumba ya Mungu vikubwa na vidogo na hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya mfalme na maofisa wake. Alivipeleka vyote mpaka Babuloni. Aliichoma moto nyumba ya Mungu, akaubomoa ukuta wa Yerusalemu, akayachoma moto majumba yote ya kifalme na kuharibu vyombo vyake vyote vya thamani. Watu walionusurika vitani aliwachukua uhamishoni Babuloni. Huko wakawa watumwa wake na wa wazawa wake mpaka mwanzo wa ufalme wa Persia. Hivyo likatimia neno la Mwenyezi-Mungu alilosema nabii Yeremia: “Nchi itabaki tupu bila kulimwa miaka sabini kulingana na muda wa pumziko ambao haukuadhimishwa.” Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi, mfalme wa Persia, ili litimie neno la Mwenyezi-Mungu alilolinena kwa njia ya nabii Yeremia, Mwenyezi-Mungu alimfanya Koreshi, mfalme wa Persia, atangaze amri ifuatayo katika ufalme wake wote na kuiweka katika maandishi: “Hivi ndivyo anavyosema Koreshi mfalme wa Persia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, amenipatia falme zote za ulimwenguni, na ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, nchini Yuda. Basi, sasa kila mtu katika nyinyi nyote mlio watu wake Mwenyezi-Mungu, Mungu wake na awe pamoja naye, na aende.” Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi, mfalme wa Persia, ili neno la Mwenyezi-Mungu alilolinena kwa njia ya nabii Yeremia litimie, Mwenyezi-Mungu alimfanya Koreshi, mfalme wa Persia, atangaze amri ifuatayo katika ufalme wake na kuiweka katika maandishi: “Hivi ndivyo anavyosema Koreshi mfalme wa Persia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, amenipatia falme zote za ulimwenguni na ameniagiza nimjengee nyumba Yerusalemu, huko Yuda. Basi sasa, kila mtu katika nyinyi nyote mlio watu wake, Mungu wake awe naye na aende Yerusalemu huko Yuda, na kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, Mungu anayeabudiwa huko Yerusalemu. Kila mmoja aliyebaki hai uhamishoni akitaka kurudi, jirani zake na wamsaidie kwa kumpa fedha, dhahabu, mali na wanyama, pamoja na matoleo ya hiari kwa ajili ya nyumba ya Mungu huko Yerusalemu.” Basi, wakaondoka viongozi wa koo za makabila ya Yuda na Benyamini, makuhani na Walawi, na kila mtu ambaye Mungu alimpa moyo wa kwenda kujenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, iliyoko Yerusalemu. Majirani waliwasaidia watu hao kwa kuwapa vyombo vya fedha, dhahabu, mali, wanyama na vitu vingine vya thamani, mbali na vile vilivyotolewa kwa hiari. Mfalme Koreshi aliwarudishia vyombo ambavyo mfalme Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuviweka katika nyumba ya miungu yake. Alimkabidhi Mithredathi, mtunza hazina, vyombo hivyo, naye akamhesabia Sheshbaza, mtawala wa Yuda. Ifuatayo ndiyo hesabu yake: Bakuli 30 za dhahabu; bakuli 1,000 za fedha; vyetezo 29; bakuli ndogo za dhahabu 30; bakuli ndogo za fedha 410; vyombo vinginevyo 1,000. Vyombo vyote vya dhahabu na fedha, pamoja na vitu vinginevyo vilikuwa jumla yake 5,400. Vyote hivi, Sheshbaza alivichukua hadi Yerusalemu wakati yeye pamoja na watu wengine alipotolewa uhamishoni Babuloni kwenda Yerusalemu. Wafuatao ni watu wa mkoani waliotoka utumwani ambao Nebukadneza mfalme wa Babuloni aliwapeleka mateka Babuloni, wakarudi mjini Yerusalemu na nchini Yuda. Kila mtu alirudi mjini kwake. Viongozi wao walikuwa Zerubabeli, Yeshua, Nehemia, Seraya, Reelaya, Mordekai, Bilshani, Mispari, Bigwai, Rehumu na Baana. Ifuatayo ni idadi ya watu wote wa koo za Israeli waliorudi kutoka uhamishoni: Wa ukoo wa Paroshi: 2,172; wa ukoo wa Shefatia: 372; wa ukoo wa Ara: 775; wa ukoo wa Pahath-moabu, yaani wazawa wa Yeshua na Yoabu: 2,812; wa ukoo wa Elamu: 1,254; wa ukoo wa Zatu: 945; wa ukoo wa Zakai: 760; wa ukoo wa Bani: 842; wa ukoo wa Bebai: 623; wa ukoo wa Azgadi: 1,222; wa ukoo wa Adonikamu: 666; wa ukoo wa Bigwai: 2,056; wa ukoo wa Adini: 454; wa ukoo wa Ateri, yaani Hezekia: 98; wa ukoo wa Besai: 323; wa ukoo wa Yora: 112; wa ukoo wa Hashumu: 223; wa ukoo wa Gibari: 95. Watu wa mji wa Bethlehemu: 123; wa mji wa Netofa: 56; wa mji wa Anathothi: 128; wa mji wa Azmawethi: 42; wa mji wa Kiriath-yearimu, wa Kefira na wa Beerothi: 743; wa mji wa Rama na wa Geba: 621; wa mji wa Mikmashi: 122; wa mji wa Betheli na Ai: 223; wa mji wa Nebo: 52; wa mji wa Magbishi: 156; wa mji wa Elamu wa pili: 1,254; wa mji wa Harimu: 320; wa mji wa Lodi, Hadidi na wa Ono: 725; wa mji wa Yeriko: 345; wa mji wa Senaa: 3,630. Ifuatayo ni idadi ya makuhani waliorudi kutoka uhamishoni: Makuhani wa ukoo wa Yedaya, waliokuwa wazawa wa Yeshua: 673; wa ukoo wa Imeri: 1,052; wa ukoo wa Pashuri: 1,247; wa ukoo wa Harimu: 1,017. Walawi wa ukoo wa Yeshua na wa Kadmieli, wazawa wa Hodavia waliorudi kutoka uhamishoni walikuwa 74. Waimbaji (wazawa wa Asafu), walikuwa 128. Walinzi (wazawa wa Shalumu, wa Ateri, wa Talmoni, wa Akubu, wa Hatita na wa Shobai), walikuwa 139. Koo za watumishi wa hekalu waliorudi kutoka uhamishoni zilikuwa: Ukoo wa Siha, wa Hasufa, wa Tabaothi, ukoo wa Kerosi, wa Siaha, wa Padoni, ukoo wa Lebana, wa Hagaba, wa Akubu, ukoo wa Hagabu, wa Shamlai, wa Hanani, ukoo wa Gideli, wa Gahari, wa Reaya, ukoo wa Resini, wa Nekoda, wa Gazamu, ukoo wa Uza, wa Pasea, wa Besai, ukoo wa Asna, wa Meunimu, wa Nefisimu, ukoo wa Bakbuki, wa Hakufa, wa Harhuri, ukoo wa Basluthi, wa Mehida, wa Harsha, ukoo wa Barkosi, wa Sisera, wa Tema, ukoo wa Nezia na wa Hatifa. Koo za wazawa wa watumishi wa Solomoni waliorudi kutoka uhamishoni zilikuwa, ukoo wa Sotai, wa Hasoferethi, wa Perudha, ukoo wa Yaala, wa Darkoni, wa Gideli, ukoo wa Shefatia, wa Hatili, wa Pokereth-hasebaimu na wa Ami. Nao watumishi wote wa hekalu na wazawa wa watumishi wa Solomoni waliorudi kutoka uhamishoni walikuwa watu 392. Watu wa miji ifuatayo, pia walirudi: Wa mji wa Tel-mela, wa Tel-harsha, wa Kerubu, wa Adani na wa Imeri, ila hawakuweza kuthibitisha kuwa walikuwa wazawa wa Waisraeli. Wao walikuwa watu wa ukoo wa Delaya wa Tobia na wa Nekoda, jumla watu 652. Watu wa koo zifuatazo za makuhani pia walirudi: Ukoo wa Habaya, wa Hakosi na wa Barzilai. Huyo Barzilai alikuwa ameoa binti Barzilai wa Gileadi, naye pia akaitwa Barzilai. Hao walitafuta orodha yao katika kumbukumbu za koo, lakini hawakuonekana humo. Kwa hiyo hawakuruhusiwa kushika ukuhani kwani walihesabiwa kuwa najisi. Mtawala akawaambia kuwa hawaruhusiwi kushiriki chakula kitakatifu sana, mpaka awepo kuhani atakayeweza kutoa kauli ya Urimu na Thumimu. Watu wote waliorudi kutoka uhamishoni jumla yao ilikuwa 42,360; mbali na hao, kulikuwa na watumishi wanaume na wanawake 7337; na walikuwa na waimbaji wanaume na wanawake, wote 200. Walikuwa na farasi 736, nyumbu 245, ngamia 435, na punda 6,720. Watu hao waliotoka uhamishoni, walipofika kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu mjini Yerusalemu, baadhi ya viongozi wa koo hizo walitoa matoleo ya hiari ili kusaidia ujenzi wa nyumba ya Mungu katika Yerusalemu. Walitoa kila mtu kadiri ya uwezo wake kwa ajili ya kazi hii. Jumla ya matoleo hayo ilikuwa kilo 500 za dhahabu, kilo 2,800 za fedha na mavazi 100 kwa ajili ya makuhani. Basi, makuhani, Walawi na baadhi ya watu wengine wakaanza kuishi mjini Yerusalemu na katika vitongoji vyake. Nao waimbaji, walinzi wa hekalu na watumishi wa hekalu wakaanza kuishi katika miji yao; Waisraeli wote waliishi katika miji yao. Baadaye mwezi wa saba ulipofika, na watu wa Israeli wakiwa wamekwisha kaa katika miji yao, wote walikusanyika pamoja mjini Yerusalemu. Yeshua, mwana wa Yosadaki, pamoja na makuhani wenzake, na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, pamoja na jamaa zake, waliijenga upya madhabahu ya Mungu wa Israeli, ili waweze kumtolea sadaka za kuteketezwa kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtu wa Mungu. Waliijenga madhabahu hiyo mahali palepale ilipokuwa hapo zamani, kwa kuwa waliwaogopa watu waliokuwa wanaishi katika nchi hiyo. Kisha wakawa wanamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa juu yake kila siku asubuhi na jioni. Waliiadhimisha sikukuu ya vibanda kama ilivyoandikwa katika sheria; kila siku walitoa sadaka za kuteketezwa zilizohitajika kwa ajili ya siku hiyo. Walitoa pia sadaka za kawaida ambazo ziliteketezwa nzima, sadaka zilizotolewa wakati wa sikukuu ya mwezi mpya na katika sikukuu nyingine zote alizoagiza Mwenyezi-Mungu. Pia, walitoa tambiko zote zilizotolewa kwa hiari. Ingawa msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu ulikuwa bado kuwekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba. Watu walitoa fedha za kuwalipa maseremala na waashi, walitoa pia chakula, vinywaji na mafuta, ili vipelekwe katika miji ya Tiro na Sidoni kupata miti ya mierezi kutoka Lebanoni. Miti hiyo ililetwa kwa njia ya bahari hadi Yopa. Haya yote yalifanyika kwa msaada wa mfalme Koreshi wa Persia. Basi, watu walianza kazi mnamo mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya kufikia nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu. Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki, ndugu zao wengine, makuhani, Walawi na watu wengine wote waliorudi Yerusalemu kutoka uhamishoni, walijiunga nao katika kazi hiyo. Walawi wote waliokuwa na umri wa miaka ishirini au zaidi, waliteuliwa ili kusimamia kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Yeshua, wanawe na jamaa yake, pamoja na Kadmieli na wanawe, (wa ukoo wa Yuda) walishirikiana kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mungu. Walisaidiwa na wazawa wa Henadadi na ndugu zao Walawi. Wajenzi walipoanza kuweka msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi, walisimama mahali pao na tarumbeta mikononi, nao Walawi wa ukoo wa Asafu wakisimama na matoazi yao; basi, walimtukuza Mwenyezi-Mungu kufuatana na maagizo ya mfalme Daudi wa Israeli. Waliimba kwa kupokezana, wakimsifu na kumtukuza Mwenyezi-Mungu: “Kwa kuwa yu mwema, fadhili zake kwa Israeli zadumu milele.” Watu wote walipaza sauti kwa nguvu zao zote, wakamsifu Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya kuanza kujengwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Wengi wa makuhani, Walawi, na viongozi wa koo waliokuwa wazee na ambao walikuwa wameiona nyumba ya kwanza, walilia kwa sauti kubwa walipouona msingi wa nyumba hii mpya unawekwa, ingawa watu wengine wengi walipaza sauti kwa furaha. Watu hawakuweza kutofautisha kati ya sauti za furaha na za kilio kwa sababu zilikuwa nyingi na zilisikika mbali sana. Kisha maadui wa watu wa Yuda na Benyamini waliposikia kwamba watu waliorudi kutoka uhamishoni wanalijenga upya hekalu la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, walimwendea Zerubabeli na viongozi wa koo, na kumwambia, “Tafadhali tushirikiane katika ujenzi wa hekalu. Sisi kama nyinyi tunamwabudu Mungu wenu, na tumekuwa tukimtolea tambiko tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru aliyetuleta hapa.” Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa koo za Israeli wakawaambia, “Sisi hatuhitaji msaada wowote kutoka kwenu ili kuijenga nyumba ya Mungu wetu. Sisi wenyewe tutamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kama mfalme Koreshi wa Persia alivyotuamuru.” Hapo, watu waliokuwa wanaishi mahali hapo wakaanza kuwavunja moyo na kuwatisha Wayahudi ili wasiendelee kama walivyokusudia. Tena waliwahonga maofisa wa serikali ya Persia wawapinge Wayahudi. Waliendelea kufanya hivyo muda wote wa utawala wa Koreshi, mpaka wakati wa utawala wa Dario. Mwanzoni mwa utawala wa mfalme Ahasuero, maadui wa watu waliokaa Yuda na Yerusalemu waliandika mashtaka dhidi yao. Tena wakati wa utawala wa Artashasta, mfalme wa Persia, Bishlamu, Mithredathi, Tabeeli na rafiki zao, walimwandikia barua mfalme Artashasta. Barua hiyo iliandikwa kwa herufi za Kiaramu na kutafsiriwa. Pia mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa, walimwandikia Artashasta barua ifuatayo dhidi ya Yerusalemu: “Kutoka kwa mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa pamoja na wenzetu, na mahakimu, maofisa wote ambao hapo awali walitoka Ereki, Babuloni na Susa katika nchi ya Elamu, pamoja na watu wa mataifa mengine ambao Asur-banipali, mtu mkuu na mwenye nguvu aliwahamisha na kuwaweka katika mji wa Samaria na mahali pengine katika mkoa wa magharibi ya Eufrate.” Barua yenyewe ilikuwa hivi: “Kwa mfalme Artashasta: Sisi watumishi wako katika mkoa wa magharibi ya Eufrate, tunakutumia salamu. Tungependa ufahamu, ewe mfalme, kwamba Wayahudi waliokuja hapa kutoka maeneo mengine ya ufalme wako wamekwenda Yerusalemu na wanaujenga upya mji huo mwasi na mwovu. Wanamalizia kujenga kuta zake na kutengeneza msingi. Tungependa ufahamu, ewe mfalme, kuwa mji huu ukijengwa upya na kuta zake zikimalizika, watu hawatalipa kodi, ushuru wala ada, na hazina yako itapungua. Sasa, kwa kuwa ni wajibu wetu, ee mfalme, hatungependa kuona ukivunjiwa heshima, ndiyo maana tumeona ni vizuri tukuarifu ili ufanye uchunguzi katika kumbukumbu za babu zako. Humo utagundua kwamba tangu zamani, mji huu ulikuwa mwasi na umewasumbua sana wafalme na watawala wa mikoa, na kuwa tangu zamani watu wake ni wachochezi sana; ndio sababu mji huo uliangamizwa. Kwa hiyo tunakujulisha kwamba ikiwa mji huu utajengwa upya na kuta zake zikimalizika, hutaweza kuutawala mkoa wa magharibi ya Eufrate.” Kisha mfalme akapeleka jibu lifuatalo: “Kwa mtawala Rehumu, kwa Shishai, katibu wa mkoa, pamoja na wenzenu wote wanaoishi Samaria na mahali penginepo katika mkoa wa magharibi ya Eufrate. “Barua mliyonitumia imetafsiriwa na kusomwa mbele yangu. Nimetoa amri uchunguzi ufanywe na imegunduliwa kuwa ni kweli kwamba tangu zamani mji huu wa Yerusalemu umekuwa ukiwapinga wafalme na kwamba watu wake wamekuwa waasi na wachochezi wakubwa. Wafalme wenye nguvu wamepata kuutawala mji huo pamoja na mkoa wa magharibi ya Eufrate wakitoza kodi, ushuru na ada. Kwa hiyo, toeni amri watu hao waache kuujenga upya mji huo hadi hapo nitakapotoa maagizo mengine. Tena, angalieni sana msichelewe kufanya hivyo, nisije nikapata hasara.” Mara tu waliposomewa barua hii kutoka kwa Artashasta, Rehumu, katibu Shimshai na wenzao waliharakisha kwenda Yerusalemu na kuwalazimisha kwa nguvu Wayahudi waache kuujenga mji. Kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu ilisimama, na hali hiyo iliendelea mpaka mwaka wa pili wa utawala wa Dario, mfalme wa Persia. Wakati huo, manabii wawili, Hagai na Zekaria, mwana wa Ido, waliwatolea unabii Wayahudi waliokuwa wanakaa Yuda na Yerusalemu, katika jina la Mungu wa Israeli. Nao Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yeshua, mwana wa Yosadaki, walipousikia ujumbe huo walianza tena kuijenga nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu, wakisaidiwa na manabii wa Mungu. Baadaye Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate, Shethar-bozenai na wenzao, walikwenda Yerusalemu na kuuliza, “Nani aliyewaamuru kuijenga nyumba hii mpaka kuimaliza?” Pia waliuliza, “Ni akina nani wanaojenga nyumba hii? Tunataka majina yao.” Lakini Mungu alikuwa anawalinda viongozi wa Wayahudi, kwa hiyo maofisa hao hawakuwakataza mpaka hapo walipomwandikia mfalme Dario na kupata maoni yake. Basi, Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate, Shethar-bozenai na wenzao, wakamwandikia mfalme Dario. Ifuatayo ni ripoti waliyompelekea mfalme: “Kwa mfalme Dario; tunakutakia amani. Tungetaka kukufahamisha ee mfalme, kuwa tulikwenda mkoani Yuda ilipo nyumba ya Mungu Mkuu. Nyumba hii inajengwa upya kwa mawe makubwamakubwa na kuta zake zinawekwa boriti za miti. Kazi hiyo inafanywa kwa uangalifu mkubwa na inaendelea vizuri sana. Tuliwauliza viongozi hao watuambie ni nani aliyewapa amri ya kuijenga upya nyumba hii mpaka kuimaliza. Tuliwauliza pia majina yao ili tuweze kukujulisha wale wanaoongoza kazi hiyo. “Wao walitujibu hivi: ‘Sisi ni watumishi wa Mungu wa mbingu na dunia, na tunaijenga upya nyumba ambayo ilikuwa imejengwa na kumalizika hapo awali na mfalme mmoja mkuu wa Israeli. Lakini kwa kuwa babu zetu walimkasirisha Mungu wa mbingu, yeye aliwatia mikononi mwa mfalme Nebukadneza wa Babuloni, Mkaldayo, aliyeiharibu nyumba hii na kuwapeleka watu uhamishoni huko Babuloni. Lakini mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wake mfalme Koreshi wa Babuloni alitoa amri nyumba hii ya Mungu ijengwe upya. Pia alivirudisha vyombo vya dhahabu na fedha ambavyo mfalme Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka katika hekalu huko Yerusalemu na kuviweka katika hekalu la Babuloni. Vyombo hivyo Koreshi aliviondoa hekaluni Babuloni na kumkabidhi Sheshbaza ambaye alikuwa amemteua awe mtawala wa Yuda; alimwamuru achukue vyombo hivyo na kuvirudisha katika hekalu la Yerusalemu, na kuijenga upya nyumba ya Mungu mahali pake. Kisha Sheshbaza alikuja na kuweka msingi wa nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu, na tangu wakati huo ujenzi umekuwa ukiendelea mpaka sasa, lakini bado haijamalizika.’ Basi, ukipenda ewe mfalme, amuru uchunguzi ufanywe katika kumbukumbu za kifalme mjini Babuloni kama mfalme Koreshi alitoa amri nyumba hii ya Mungu ijengwe upya mjini Yerusalemu. Kisha, tunakuomba utujulishe maoni yako kuhusu jambo hili.” Mfalme Dario alitoa amri na uchunguzi ulifanywa mjini Babuloni katika nyumba ya kumbukumbu za kifalme. Lakini kitabu kilipatikana mjini Ekbatana katika mkoa wa Media, nacho kilikuwa na maagizo yafuatayo: “Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wake, mfalme Koreshi alitoa amri nyumba ya Mungu ijengwe upya mjini Yerusalemu, na iwe mahali pa kutolea tambiko na sadaka za kuteketezwa. Kimo chake kitakuwa mita 27 na upana wake mita 27. Kuta zake zitajengwa kwa safu moja ya miti juu ya kila safu tatu za mawe makubwa. Gharama zote zilipwe kutoka katika hazina ya mfalme. Pia, vyombo vyote vya dhahabu na fedha ambavyo mfalme Nebukadneza alivileta Babuloni kutoka katika hekalu la Yerusalemu, vitarudishwa na kuwekwa kila kimoja mahali pake katika nyumba ya Mungu.” Ndipo Dario akapeleka ujumbe ufuatao: “Kwa Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate, Shethar-bozenai na maofisa wenzako mkoani. ‘Msiende huko kwenye hekalu, na acheni kazi ya ujenzi wa nyumba hii ya Mungu iendelee. Mwacheni mtawala wa Yuda na viongozi wa Wayahudi waijenge nyumba ya Mungu mahali pake. Zaidi ya hayo, natoa amri kwamba nyinyi mtawasaidia katika kazi hiyo. Gharama zao zote zitalipwa bila kuchelewa kutoka katika hazina ya mfalme inayotokana na kodi kutoka katika mkoa wa magharibi wa mto Eufrate. Kila siku, tena bila kukosa, mtawapa makuhani wa Yerusalemu kila kitu watakachohitaji; iwe ni fahali wachanga, kondoo dume au wanakondoo wa sadaka za kuteketezwa kwa Mungu wa mbinguni, au ngano, chumvi, divai au mafuta. Haya yote yatatendeka ili waweze kumtolea Mungu wa mbinguni tambiko zinazompendeza na waombee maisha yangu mimi mfalme na watoto wangu. Naamuru pia kwamba mtu yeyote ambaye hatatii amri hii, boriti ingolewe kutoka katika nyumba yake, na atumbuliwe kwayo. Tena, nyumba yake na ifanywe kuwa rundo la mavi. Mungu aliyeuchagua mji wa Yerusalemu kuwa mahali pake pa kuabudiwa na amwangushe mfalme au taifa lolote litakalopinga amri hii au kutaka kuiharibu nyumba hii ya Mungu iliyoko mjini Yerusalemu. Mimi Dario nimetoa amri hii. Ni lazima ifuatwe.’” Basi, Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate, Shethar-bozenai, na maofisa wenzao, wakafanya bidii kutekeleza maagizo ya mfalme. Viongozi wa Wayahudi waliendelea vizuri sana na kazi ya ujenzi wa hekalu, wakitiwa moyo kwa mahubiri ya nabii Hagai na Zekaria, mwana wa Ido. Walimaliza ujenzi wa hekalu kama walivyoamriwa na Mungu wa Israeli, na kama walivyoagizwa na mfalme Koreshi, mfalme Dario na mfalme Artashasta, wa Persia. Ujenzi wa nyumba hiyo ulimalizika mnamo siku ya tatu ya mwezi wa Adari, katika mwaka wa sita wa utawala wa mfalme Dario. Basi, watu wa Israeli, makuhani, Walawi na watu wengine waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni waliiweka wakfu nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa shangwe kuu. Wakati wa kuiweka wakfu nyumba ya Mungu, walitoa mafahali 100, kondoo madume 200, wanakondoo 800 na mbuzi madume 12 kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, mbuzi mmoja kwa kila kabila la Israeli. Pia, kwa ajili ya huduma ya Mungu katika Yerusalemu, waliwapanga makuhani katika makundi yao ya Walawi katika zamu zao kufuatana na maagizo yaliyoandikwa katika kitabu cha Mose. Mnamo siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, watu waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni walisherehekea Pasaka. Makuhani na Walawi walikuwa wamejitakasa, wote walikuwa safi kabisa. Walichinja mwanakondoo wa Pasaka kwa ajili ya watu wote waliorudi kutoka uhamishoni, ndugu zao makuhani na kwa ajili yao wenyewe. Waliokula mwanakondoo wa Pasaka walikuwa Waisraeli wote waliorudi kutoka uhamishoni pamoja na watu wengine wote ambao walikuwa wameziacha njia za mataifa mengine ili kumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Kwa muda wa siku saba watu walisherehekea kwa furaha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, kwa sababu Mwenyezi-Mungu aliwajalia furaha na kumpa mfalme wa Ashuru moyo wa upendo kwao, akawasaidia katika kazi za ujenzi wa nyumba ya Mungu wa Israeli. Baadaye, wakati wa utawala wa mfalme Artashasta wa Persia, palikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Ezra. Ezra alikuwa mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia, mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu, mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi, mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki, mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Aroni, kuhani mkuu. Ezra aliondoka Babuloni, yeye alikuwa mwandishi mwenye ujuzi mwingi sana katika sheria ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alikuwa amempatia Mose. Na kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, mfalme alimpatia Ezra kila kitu alichohitaji. Mnamo mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Artashasta, Ezra alifunga safari kutoka Babuloni kwenda Yerusalemu. Baadhi ya watu wa Israeli, makuhani, Walawi, waimbaji, walinda malango na wahudumu wa hekalu walikwenda pamoja naye. Waliwasili mjini Yerusalemu mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Artashasta. Mwenyezi-Mungu aliifanikisha sana safari yao waliyokuwa wameianza siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza. Ezra alikuwa amejitoa kwa moyo wote kujifunza sheria ya Mwenyezi-Mungu, kuitii na kuwafundisha watu wa Israeli maagizo na amri zake. Ifuatayo ni barua ambayo Artashasta alimpa Ezra, kuhani na mwandishi, na mwenye ujuzi katika amri na masharti ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa watu wa Israeli. “Kutoka kwa Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani na mtu mwenye ujuzi katika sheria ya Mungu wa mbinguni; Wasalaam!” “Ninaamuru kwamba katika utawala wangu, Mwisraeli yeyote, au kuhani wao, au Mlawi, akitaka kurudi Yerusalemu kwa hiari yake, anaweza kwenda pamoja nawe. “Mimi pamoja na washauri wangu saba, tunakutuma uende ufanye uchunguzi huko Yuda na Yerusalemu kuona kama sheria ya Mungu wako ambayo umekabidhiwa inafuatwa kikamilifu. Utachukua fedha na dhahabu ambayo mimi na washauri wangu tumemtolea kwa hiari Mungu wa Israeli ambaye hekalu lake limo mjini Yerusalemu. Utachukua pia fedha na dhahabu yote utakayokusanya katika mkoa wote wa Babuloni, pamoja na matoleo ya hiari waliyotoa Waisraeli na makuhani wao kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu. Fedha hiyo utaitumia kwa uangalifu sana kununua mafahali, kondoo dume, wanakondoo na tambiko ya nafaka na divai, na kuvitoa madhabahuni katika nyumba ya Mungu wenu iliyoko Yerusalemu. Fedha na dhahabu itakayobaki unaweza kuitumia pamoja na wananchi wenzako kama mtakavyopenda, kufuatana na mapenzi ya Mungu. Vyombo ambavyo umekabidhiwa kwa ajili ya ibada ya nyumba ya Mungu wako, utamtolea Mungu wa Yerusalemu. Ukihitaji kitu kingine chochote kwa ajili ya nyumba ya Mungu wako unaweza kukipata kutoka katika hazina ya mfalme. Mimi mfalme Artashasta, natoa amri kwa waweka hazina wote katika mkoa wa magharibi ya mto Eufrate kwamba chochote atakachohitaji Ezra, kuhani na mwandishi wa sheria ya Mungu wa mbinguni, mtampa, tena bila kusita, fedha kiasi atakacho mpaka kufikia kilo 3,400, ngano kilo 10,000, divai lita 2,000, mafuta lita 2,000, na chumvi kiasi chochote atakachohitaji. Kila kitu alichoagiza Mungu wa mbinguni kwa ajili ya nyumba yake, ni lazima kitekelezwe kikamilifu, asije akaukasirikia ufalme wangu au wanangu. Tunawafahamisheni pia kuwa ni marufuku kuwadai kodi ya mapato, ushuru au ada makuhani, Walawi, waimbaji, walinda mlango, wafanyakazi au watumishi wengine wa nyumba hii ya Mungu. Nawe Ezra, kwa kutumia hekima aliyokupa Mungu wako, hiyo uliyonayo, chagua mahakimu, na waamuzi watakaowaongoza wakazi wote wa mkoa wa magharibi ya Eufrate ambao wanaishi kufuatana na sheria ya Mungu wako. Na yule ambaye haijui sheria hiyo, mfundishe. Mtu yeyote ambaye hatatii sheria ya Mungu wako na ya mfalme, na ahukumiwe mara moja: Kufa, kuhamishwa, kunyanganywa mali yake au kufungwa.” Ezra akasema, “Na asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zetu; ambaye amempatia mfalme moyo wa kutia mapambo nyumba ya Mwenyezi-Mungu iliyoko Yerusalemu. Kwa fadhili zake Mungu, nimepata msaada wa mfalme na maofisa wake wenye uwezo mkuu. Nilijipa moyo kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, alikuwa pamoja nami, hata niliwakusanya viongozi wa Israeli ili warudi pamoja nami.” Ifuatayo ni orodha ya viongozi wa koo za watu waliorudi pamoja nami Ezra kutoka Babuloni, wakati wa utawala wa mfalme Artashasta: Gershomu, wa ukoo wa Finehasi. Danieli, wa ukoo wa Ithamari. Hatushi, wa ukoo wa Daudi, aliyekuwa mwana wa Shekania. Zekaria, wa ukoo wa Paroshi, pamoja na wanaume 150 wa ukoo wake, walioandikishwa pamoja. Eliehoenai, mwana wa Zerahia, wa ukoo wa Pahath-moabu, pamoja na wanaume 200. Shekania, mwana wa Yahazieli, wa ukoo wa Zatu, pamoja na wanaume 300. Ebedi, mwana wa Yonathani, wa ukoo wa Adini, pamoja na wanaume 50. Yeshaya, mwana wa Athalia, wa ukoo wa Elamu, pamoja na wanaume 70. Zebadia, mwana wa Mikaeli, wa ukoo wa Shefatia, pamoja na wanaume 80. Obadia, mwana wa Yehieli, wa ukoo wa Yoabu, pamoja na wanaume 218. Shelomithi, mwana wa Yosifia, wa ukoo wa Bani, pamoja na wanaume 160. Zekaria, mwana wa Bebai, wa ukoo wa Bebai, pamoja na wanaume 28. Yohanani, mwana wa Hakatani, wa ukoo wa Azgadi, pamoja na watu 110. Elifeleti, Yeueli na Shemaya, wa ukoo wa Adonikamu, pamoja na wanaume 60, (hawa walirudi baadaye). Uthai na Zakuri, wa ukoo wa Bigwai, pamoja na wanaume 70. Niliwakusanya pamoja watu wote kando ya mto uelekeao mji wa Ahava. Huko, tulipiga kambi kwa muda wa siku tatu. Niliwakagua watu wote pamoja na makuhani, lakini sikupata Walawi miongoni mwao. Niliita waje kwangu viongozi tisa: Eliezeri, Arieli, Shemaya, Elnathani, Yaribu, Elnathani, Nathani, Zekaria na Meshulamu, pamoja na waalimu wawili, Yoyaribu na Elnathani. Nikawatuma kwa Ido, kiongozi wa jamii ya watu kule Kasifia, nikimwomba yeye pamoja na wenzake wahudumu wa nyumba ya Mungu, watuletee watu watakaohudumu katika nyumba ya Mungu. Kwa neema yake Mungu, walituletea Sherebia, mtu mwenye busara na Mlawi wa ukoo wa Mahli, pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wanane. Walituletea pia Hashabia na Yeshaya, wote wa ukoo wa Merari, pamoja na ndugu zao ishirini. Mbali na hao, kulikuwa na wahudumu wa hekalu 220 ambao babu zao walikuwa wamechaguliwa na mfalme Daudi na maofisa wake kuwasaidia Walawi. Majina ya watu wote hawa yaliorodheshwa. Kisha, nilitoa maagizo kuwa sote tufike karibu na mto Ahava ili tufunge na kujinyenyekeza mbele za Mungu wetu na kumwomba atulinde na kutuongoza katika safari yetu pamoja na watoto wetu. Ingekuwa aibu kubwa kwangu kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapandafarasi wa kutulinda na adui njiani maana nilikuwa nimekwisha mwambia kuwa Mungu wetu huwabariki wote wanaomtafuta, lakini huwachukia na kuwaadhibu wote wanaomwacha. Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu atulinde, naye aliyasikia maombi yetu. Halafu kati ya makuhani waliokuwa viongozi nilichagua kumi na wawili: Sherebia, Hashabia pamoja na wenzao kumi. Hawa niliwapimia kwa mizani fedha, dhahabu na vyombo ambavyo mfalme, washauri wake, maofisa wake pamoja na watu wa Israeli walivyokuwa wamevitoa kwa ajili ya sadaka ya nyumba ya Mungu wetu. Hivi ndivyo vitu nilivyowapimia: Fedha tani 22, vyombo 100 vya fedha, uzito wake kilo 70, dhahabu kilo 3400, mabakuli 20 ya dhahabu, uzito wake kilo 8, vyombo viwili vya shaba nzuri iliyongaa yenye thamani kama ya dhahabu. Kisha nikawaambia, “Nyinyi ni wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Kadhalika vyombo ni wakfu na fedha na dhahabu ni matoleo ya hiari kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu. Tafadhali vilindeni na vitunzeni mpaka mtakapovipima mbele ya makuhani wakuu, Walawi na viongozi wa koo za Israeli, huko Yerusalemu katika vyumba vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Basi, makuhani na Walawi wakachukua fedha, dhahabu na vyombo vyote walivyopimiwa, ili kuvipeleka mjini Yerusalemu katika nyumba ya Mungu wetu. Mnamo siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza, tulisafiri kutoka mto Ahava, kwenda Yerusalemu. Mungu wetu alikuwa pamoja nasi, akatulinda na maadui na washambuliaji wa njiani. Tulipofika Yerusalemu, tulipumzika kwa muda wa siku tatu. Mnamo siku ya nne, tukiwa ndani ya nyumba ya Mungu wetu, tulipima ile fedha, dhahabu na vile vyombo, kisha tukamkabidhi kuhani Meremothi, mwana wa Uria. Meremothi alikuwa pamoja na Eleazari, mwana wa Finehasi, na Walawi wawili, Yozabadi, mwana wa Yeshua, na Noadia, mwana wa Binui. Kila kitu kilihesabiwa na kupimwa na wakati huo uzito wa kila kitu uliandikwa. Kisha, watu wote waliorudi kutoka uhamishoni walimtolea Mungu wa Israeli sadaka zao za kuteketezwa. Walitoa mafahali 12 kwa ajili ya Israeli yote, kondoo madume 96 na wanakondoo 77; pia walitoa mbuzi 12 kama sadaka ya kuondoa dhambi. Wanyama wote hawa walitolewa kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi-Mungu. Aidha, waliwakabidhi manaibu wa mfalme na watawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate mwongozo waliopewa na mfalme, nao walitoa msaada kwa watu na kwa ajili ya nyumba ya Mungu. Baada ya mambo haya yote kutendeka, viongozi walinijia na kunipa taarifa ifuatayo: “Watu wa Israeli, makuhani na Walawi hawajajitenga na wakazi wa nchi ambao wanatenda machukizo: Waamoni, Wamoabu na Wamisri, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wayebusi na Waamori. Wayahudi wanaoa wanawake wa kigeni na kuwaoza wavulana wao pia. Hivyo, taifa takatifu la Mungu limechanganyika na watu wa mataifa mengine Isitoshe, maofisa na wakuu ndio wa kwanza kutenda maovu hayo.” Nilipoyasikia maelezo hayo, nilizirarua nguo zangu na joho langu, nikazingoa nywele zangu na ndevu zangu kwa huzuni kubwa na kuketi chini kwa hofu. Ndipo watu wote walioshikwa na hofu kwa sababu ya maneno aliyosema Mungu wa Israeli kuhusu makosa ya wale waliorudi kutoka uhamishoni walipoanza kukusanyika karibu nami hali nikikaa katika hofu hadi jioni, wakati wa kutoa tambiko. Jioni, wakati wa kutoa tambiko ulipofika, niliinuka mahali hapo nilipokuwa nimekaa kwa huzuni huku nguo zangu zimeraruka pamoja na joho, nikapiga magoti na kumnyoshea mikono yangu Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, na kuomba, nikisema, “Ee Mungu wangu, naona aibu kubwa sana kukiinua kichwa changu mbele yako. Dhambi zetu zimerundikana kupita hata vichwa vyetu; naam, makosa yetu yanafika hata mbinguni. Tangu nyakati za babu zetu hadi sasa, sisi watu wako tumekukosea sana. Na kwa sababu ya dhambi zetu, sisi, wafalme wetu na makuhani wetu tumetiwa mikononi mwa wafalme wa nchi za kigeni, tukauawa, tukachukuliwa mateka na kunyanganywa mali zetu. Na hadi hivi leo, tumetiwa haya kupita kiasi. Lakini sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa muda mfupi umetuonesha huruma yako na kuwawezesha baadhi yetu kuponyoka kutoka utumwani na kuishi kwa usalama mahali hapa patakatifu. Badala ya utumwa, umetupa furaha na maisha mapya. Hukutuacha tuishi utumwani ingawa tulikuwa tu watumwa Uliwafanya wafalme wa Persia wawe wema kwetu na kuturuhusu tuishi na kuijenga nyumba yako iliyokuwa imebomoka, ukatufanya tukae salama hapa Yuda na Yerusalemu. “Lakini sasa, ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo yote? Maana, tumeziasi amri zako ulizotupa kwa njia ya watumishi wako manabii ukisema: ‘Nchi mnayoiendea na ambayo itakuwa mali yenu ni nchi iliyo najisi yenye uchafu wa wakazi toka nchi mbalimbali, kwa machukizo yao, wameijaza unajisi tele kila mahali. Kwa hiyo, msiwaoze watu hao binti zenu, wala msiwaruhusu wavulana wenu kuwaoa binti zao. Pia, msishughulikie usalama au mafanikio yao, ili nyinyi wenyewe muweze kuwa na nguvu, na mfaidi mema ya nchi hiyo na kuwaachia watoto wenu kama urithi milele.’ Hata baada ya yote yaliyotupata kwa sababu ya maovu yetu na makosa yetu mengi, tunajua kwamba adhabu uliyotupa, ee Mungu wetu, ni ndogo ikilinganishwa na makosa yetu, na umewaacha baadhi yetu hai. Je, tutavunja amri zako tena na kuoana na watu hawa watendao maovu haya? Je, hutatukasirikia na kutuangamiza kabisa, asibaki hata mmoja wetu hai wala yeyote wa kutoroka? Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki na umetuacha tubaki kama tulivyo hivi leo. Tunaungama makosa yetu mbele yako, tukijua kuwa hakuna aliye na haki yoyote ya kuja mbele yako kwa ajili ya makosa haya.” Wakati Ezra alipokuwa anaomba na kuungama huku analia na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, umati mkubwa wa watu wa Israeli, wanaume, wanawake na watoto, walikusanyika karibu naye wakilia kwa uchungu mwingi. Ndipo Shekania, mwana wa Yehieli, wa ukoo wa Elamu, akamwambia Ezra, “Tumekosa uaminifu kwa Mungu kwa kuoa wanawake wa kigeni wa nchi hii, lakini hata hivyo bado kuna tumaini kwa ajili ya Israeli. Kwa hiyo, na tufanye agano na Mungu wetu, tuachane na wanawake hawa pamoja na watoto wao, kwa kufuatana na ushauri wako na wa wengine wanaotii amri za Mungu. Yote yatendeke kwa kufuatana na sheria. Amka uchukue hatua, sisi tutakuunga mkono. Kwa hiyo jipe moyo ufanye hivyo.” Ezra alianza kwa kuwafanya makuhani, viongozi, Walawi na Waisraeli wengine wote waape kwamba watafanya kama ilivyosemwa, nao wakakubali kula kiapo. Kisha, Ezra akaondoka mbele ya nyumba ya Mungu, akaenda nyumbani kwa Yehohanani, mwana wa Eliashibu. Huko, Ezra alilala usiku kucha bila kula wala kunywa maji, kwa huzuni aliyokuwa nayo juu ya ukosefu wa imani ya watu waliotoka uhamishoni. Tangazo lilitolewa kila mahali nchini Yuda na mjini Yerusalemu kwa wote waliotoka uhamishoni kuwa wakusanyike Yerusalemu. Ikiwa mtu yeyote atashindwa kufika katika muda wa siku tatu, kulingana na amri iliyotolewa na viongozi, mali yake yote itachukuliwa, naye binafsi atapigwa marufuku kujiunga na jumuiya ya watu waliorudi kutoka uhamishoni. Katika siku hizo tatu, mnamo siku ya ishirini ya mwezi wa tisa, watu wote walioishi katika Yuda na Benyamini walifika Yerusalemu na kukusanyika katika uwanja wa nyumba ya Mungu. Watu wote walikuwa wakitetemeka kwa sababu ya jambo waliloitiwa na kwa ajili ya mvua nyingi iliyokuwa ikinyesha. Kuhani Ezra alisimama kuzungumza na watu, akawaambia: “Hamkuwa waaminifu kwa kuoa wanawake wa kigeni, na hivyo mmeiongezea Israeli hatia. Sasa, tubuni dhambi zenu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, na kufanya yale yanayompendeza. Jitengeni na wakazi wa nchi hii na kuwaacha wake zenu wa kigeni.” Watu wote walipaza sauti na kujibu kwa pamoja, “Ni sawa! Ni lazima tufanye kama unavyosema.” Lakini wakaongeza kusema, “Watu ni wengi na mvua inanyesha sana. Hatuwezi kuendelea kusimama hapa uwanjani, na hili si jambo ambalo litamalizika kwa siku moja au mbili! Tumefanya kosa kubwa sana kuhusu jambo hili. Afadhali maofisa wetu wabaki Yerusalemu kushughulikia jambo hili kwa niaba ya watu wote. Kisha, kila mmoja ambaye ameoa mwanamke wa kigeni na aje kwa zamu pamoja na viongozi na mahakimu wa mji wake, mpaka hapo ghadhabu kali ya Mungu wetu itakapoondolewa kwetu.” Hakuna aliyepinga mpango huu, ila Yonathani, mwana wa Asaheli na Yazeya, mwana wa Tikwa, nao wakaungwa mkono na Meshulamu na Mlawi Shabethai. Watu wote waliorudi kutoka uhamishoni walikubali mpango huo, kwa hiyo kuhani Ezra aliwachagua wanaume kati ya viongozi wa koo mbalimbali na kuyaorodhesha majina yao. Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, watu hao walianza kazi yao ya uchunguzi wa jambo hilo. Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, walikuwa wamekwisha maliza uchunguzi wao kuhusu wanaume wote waliokuwa wameoa wanawake wa kigeni. Hii ndiyo orodha ya wanaume waliokuwa wameoa wanawake wa kigeni: Makuhani kulingana na koo zao: Ukoo wa Yeshua, mwana wa Yehosadaki na ndugu zake: Maaseya, Eliezeri, Yaribu na Gedalia. Hao waliahidi kuwaacha wake zao, na wakatoa kondoo dume kuwa sadaka kwa ajili ya hatia yao. Ukoo wa Imeri: Hanani na Zebadia. Ukoo wa Harimu: Maaseya, Elia, Shemaya, Yehieli na Uzia. Ukoo wa Pashuri: Eliehoenai, Maaseya, Ishmaeli, Nethaneli, Yozabadi na Elasa. Walawi: Yozabadi, Shimei, Kelaya (aliyejulikana pia kama Kelita), Pethahia, Yuda na Eliezeri. Kati ya waimbaji: Eliashibu. Walinzi wa hekalu: Shalumu, Telemu na Uri. Watu wengineo wa Israeli: Ukoo wa Paroshi: Ramia, Izia, Malkiya, Miyamini, Eleazari, Malkiya na Benaya. Ukoo wa Elamu: Matania, Zekaria, Yehieli, Abdi, Yeremothi na Elia. Ukoo wa Zatu: Eliehoenai, Eliashibu, Matania, Yeremothi, Zabadi na Aziza. Ukoo wa Bebai: Yehohanani, Hanania, Zabai na Athlai. Ukoo wa Bani: Meshulamu, Maluki, Adaya, Yashubu, Sheali na Yeremothi. Ukoo wa Pahath-moabu: Adna, Kelali, Benaya, Maaseya, Matania, Besaleli, Binui na Manase. Ukoo wa Harimu: Eliezeri, Ishiya, Malkiya, Shemaya, Shimeoni, Benyamini, Maluki na Shemaria. Ukoo wa Hashumu: Matenai, Matata, Zabadi, Elifeleti, Yeremai, Manase na Shimei. Ukoo wa Bani: Maadai, Amramu, Ueli, Benaya, Bedeya, Keluhi, Wania, Meremothi, Eliashibu, Matania, Matenai na Yaasu. Ukoo wa Binui: Shimei, Shelemia, Nathani, Adaya, Maknadebai, Shashai, Sharai, Azareli, Shelemia, Shemaria, Shalumu, Amaria na Yosefu. Ukoo wa Nebo: Yeieli, Matithia, Zabadi, Zebina, Yadai, Yoeli na Benaya. Wanaume hawa wote walikuwa wameoa wanawake wa kigeni. Basi wakawaacha wanawake hao pamoja na watoto wao. Lifuatalo ni simulizi la Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa, nilipokuwa katika mji mkuu wa Susa, katika mwezi wa Kislevu wa mwaka wa ishirini, Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akaja pamoja na baadhi ya watu toka nchini Yuda. Nikawauliza kuhusu Wayahudi wenzetu waliosalimika, yaani ambao hawakuhamishiwa Babuloni na kuhusu mji wa Yerusalemu. Wao wakaniambia, “Wayahudi waliosalimika na kubaki katika mkoa ule, wako katika taabu na aibu. Ukuta wa mji wa Yerusalemu umebomolewa na malango yake yameteketea.” Niliposikia hayo nilikaa chini na kulia, nikaomboleza kwa siku kadhaa. Nikafunga na kumwomba Mungu wa mbinguni, nikisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbinguni, wewe u Mungu aliye mkuu na wa kutisha, unalishika agano lako na unawafadhili wale wakupendao na kuzishika amri zako. Yasikilize kwa makini maombi yangu, na uniangalie mimi mtumishi wako, ninapokuomba kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli, usiku na mchana. Ninaungama dhambi za watu wa Israeli, tulizofanya mbele yako. Mimi pamoja na watu wa jamaa yangu tumefanya dhambi. Tumetenda mabaya mbele yako, hatujazishika amri zako, kanuni na maagizo yako uliyomwagiza mtumishi wako Mose. Kumbuka sasa lile ulilomwambia mtumishi wako Mose, uliposema, ‘Kama hamtakuwa waaminifu, nitawatawanya miongoni mwa mataifa. Lakini mkinirudia, mkazishika amri zangu na kuzifuata hata ingawa nitakuwa nimewatawanya mbali kabisa, nitawarudisha mahali nilipochagua kuwa mahali pangu pa kuabudiwa.’ Watu wa Israeli ni watumishi wako na watu wako uliwakomboa kwa uwezo wako na mkono wako wenye nguvu. Ee Bwana, yasikie maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watumishi wako wanaofurahia kukutii wewe. Nakuomba unifanikishe leo, mimi mtumishi wako, na kunijalia kuhurumiwa na mfalme.” Basi, mimi nilikuwa na jukumu la kumpa mfalme kinywaji. Katika mwezi wa Nisani, katika mwaka wa ishirini wa utawala wa mfalme Artashasta, wakati divai ilipokuwa mbele yake, nilichukua divai na kumpelekea mkononi mwake. Kamwe sikuwahi kuwa mwenye huzuni mbele yake. Mfalme Artashasta akaniuliza, “Je, mbona unaonekana kuwa mwenye huzuni, ingawa huonekani kuwa mgonjwa? Naona una huzuni sana moyoni mwako!” Ndipo nilipoogopa sana. Nikamjibu, “Ee mfalme, udumu milele! Kwa nini nisiwe mwenye huzuni wakati mji wa Yerusalemu yalimo makaburi ya babu zangu uko tupu na malango yake yameteketezwa kwa moto?” Ndipo mfalme Artashasta akanijibu, “Sasa unaomba nini?” Nikamwomba Mungu wa mbinguni. Halafu nikamwambia mfalme, “Ee mfalme, ikiwa unapendezwa nami na ikiwa nimepata upendeleo mbele yako, nakuomba unitume Yuda ili niende kuujenga upya mji ambamo yamo makaburi ya babu zangu.” Mfalme akaniuliza (malkia akiwa karibu naye), “Utakuwa huko kwa muda gani na utarudi lini hapa?” Ombi langu akalikubali nami nikamjulisha wakati nitakaporudi. Nikamjibu, “Ee mfalme ikiwa unapendezwa nami, naomba nipewe barua ili nizipeleke kwa watawala wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate ili waniruhusu nipite hadi nchini Yuda. Pia nakuomba barua iandikwe kwa Asafu mtunzaji wa msitu wa kifalme ili anipatie mbao za kutengenezea miimo ya malango ya ngome ya hekalu, ukuta wa mji na nyumba yangu nitakamokaa.” Mfalme akakubali ombi langu kwa kuwa Mungu, kwa wema wake, alikuwa pamoja nami. Nilipowafikia wakuu wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate, niliwapa barua za mfalme. Mfalme alikuwa amenituma pamoja na maofisa wa jeshi na wapandafarasi. Lakini Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, Mwamoni, mtumishi wake, waliposikia kuwa nimekuja ili kushughulikia hali njema ya watu wa Israeli, hawakufurahia kabisa jambo hilo. Hivyo nikafika Yerusalemu, nikakaa huko kwa siku tatu. Kisha niliondoka usiku, mimi pamoja na watu wachache; sikumwambia mtu yeyote yale ambayo Mungu alikuwa ameyaweka moyoni mwangu kwa ajili ya mji wa Yerusalemu. Lakini siku moja usiku, niliondoka na kuwachukua watu wachache tu. Sikuchukua mnyama yeyote isipokuwa punda niliyempanda mimi mwenyewe. Nikatoka nikipitia Lango la Bondeni katika njia ielekeayo kwenye Kisima cha Joka na Lango la Mavi; nikazikagua kuta za mji wa Yerusalemu ambazo zilikuwa zimebomolewa pamoja na malango yake ambayo yalikuwa yameteketezwa kwa moto. Halafu, nikaenda kwenye Lango la Chemchemi na kwenye Bwawa la Mfalme. Lakini yule punda niliyempanda hakuweza kupita. Wakati huo wa usiku, nikapitia bondeni na kukagua ukuta wa mji. Nilirudi nikapitia Lango la Bondeni. Maofisa hawakujua mahali nilipokuwa nimekwenda wala nimefanya nini. Tena nilikuwa sijawaambia Wayahudi, makuhani, viongozi, wakuu wala wale watu ambao wangeifanya kazi ya kuujenga upya mji. Kisha nikawaambia, “Bila shaka mnaliona tatizo letu kuwa mji wa Yerusalemu ni magofu na malango yake yameteketezwa kwa moto. Basi, na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu ili tusiaibishwe zaidi.” Nikawaeleza jinsi Mungu alivyokuwa pamoja nami akinitendea kwa wema wake. Nikawaeleza pia maneno ambayo mfalme alikuwa ameniambia. Wao walipoyasikia hayo, wakasema, “Haya, na tuanze kazi ya ujenzi.” Hivyo wakajiandaa kwa kazi hiyo njema. Lakini Sanbalati, Mhoroni, Tobia, Mwamoni mtumishi wake, na Geshemu, Mwarabu, waliposikia, wakatucheka na kutuzomea wakisema, “Ni kitu gani hiki mnachotenda? Je, mnataka kumwasi mfalme?” Nikawajibu, “Mungu wa mbinguni atatufanikisha katika kazi hii, nasi tulio watumishi wake tutaanza ujenzi. Lakini nyinyi hamna fungu wala haki wala kumbukumbu katika mji wa Yerusalemu.” Basi Lango la Kondoo lilijengwa upya na Eliashibu, kuhani mkuu, pamoja na ndugu zake waliokuwa makuhani. Waliliweka wakfu na kutia milango yake; wakaliweka wakfu tangu Mnara wa Mia Moja hadi Mnara wa Hananeli. Sehemu iliyofuata ilijengwa upya na watu wa mji wa Yeriko. Baada ya hayo akafuata Zakuri mwana wa Imri kujenga ukuta. Lango la Samaki lilijengwa upya na ukoo wa Hasena, wakatia miimo yake, milango, bawaba na makomeo yake. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Meshulamu, mwana wa Berekia, mwana wa Meshezabeli. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Sadoki, mwana wa Baana. Sehemu inayofuata ilijengwa na watu kutoka mji wa Tekoa. Lakini viongozi wa mji wakakataa kufanya kazi ya mikono waliyoagizwa kufanya na wasimamizi. Lango la Zamani lilijengwa upya na Yoyada, mwana wa Pasea, pamoja na Meshulamu, mwana wa Besodeya, wakatia miimo yake, milango, bawaba na makomeo yake. Waliowafuata hao katika kazi hiyo ya kujenga upya walikuwa Melatia, Mgibeoni; Yadoni, Mmeronothi pamoja na watu wa mji wa Gibeoni na Mizpa waliokuwa chini ya uongozi wa mtawala wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate. Sehemu inayofuata, ilijengwa upya na Uzieli, mwana wa Harkaya, mfua dhahabu. Sehemu inayofuata hadi Ukuta Mpana ilijengwa upya na Hanania, mtengenezaji wa marashi. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Refaya, mwana wa Huri, mkuu wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu. Sehemu inayofuata, inayokabiliana na nyumba yake ilijengwa upya na Yedaya, mwana wa Harumafu. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Hatushi, mwana wa Hashabneya. Sehemu inayofuata pamoja na Mnara wa Tanuri vilijengwa upya na Malkiya, mwana wa Harimu akishirikiana na Hashubu, mwana wa Pahath-moabu. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Shalumu, mwana wa Haloheshi, mtawala wa nusu nyingine ya wilaya ya Yerusalemu. Alisaidiana na binti zake katika ujenzi huo. Lango la Bondeni lilijengwa upya na Hanuni pamoja na wakazi wa mji wa Zanoa. Wakayaweka malango mahali pake, wakatia bawaba na makomeo yake. Waliujenga upya ukuta ukiwa na urefu wa mita 400 hivi hadi Lango la Samadi. Lango la Samadi lilijengwa upya na Malkiya, mwana wa Rekabu, mkuu wa wilaya ya Beth-hakeremu. Akaliweka lango mahali pake, akatia bawaba na makomeo yake. Lango la Chemchemi lilijengwa upya na Shalumu, mwana wa Kolhoze, mkuu wa wilaya ya Mizpa. Akalifunika, akaliweka lango mahali pake, akatia bawabu na makomeo yake. Kwenye Bwawa la Shela akajenga ukuta ulio karibu na bustani ya kifalme hadi ngazi zinazoshuka toka mji wa mfalme Daudi. Sehemu inayofuata hadi kwenye makaburi ya Daudi, bwawa na majengo ya jeshi ilijengwa upya na Nehemia, mwana wa Azbuki, mkuu wa nusu ya wilaya ya Beth-suri. Baada ya hao, Walawi waliendeleza ujenzi mpya wa ukuta. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Rehumu, mwana wa Bani, na Hashabia, mkuu wa nusu ya wilaya ya Keila, alijenga upya sehemu inayohusu wilaya yake. Baada ya huyo, sehemu zinazofuata zilijengwa upya na ndugu zao. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Bavai, mwana wa Henadadi, mkuu wa nusu ya wilaya ya Keila. Sehemu inayofuata inayoelekeana na ghala ya silaha kwenye pembe ya ukuta ilijengwa upya na Ezeri, mwana wa Yeshua, mkuu wa Mizpa. Sehemu inayofuata tangu pembeni hadi kwenye mlango wa Eliashibu, kuhani mkuu, ilijengwa upya na Baruku, mwana wa Zabai. Sehemu inayofuata tangu mlangoni mwa nyumba ya Eliashibu, kuhani mkuu, hadi mwisho wa nyumba hiyo, ilijengwa upya na Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na makuhani waliokaa katika sehemu tambarare. Benyamini na Hashubu walijenga upya sehemu inayokabiliana na nyumba yake. Azaria, mwana wa Maaseya, mwana wa Anania, alijenga upya sehemu inayokabiliana na nyumba yao. Kuanzia kwenye nyumba ya Azaria hadi pembeni mwa ukuta ilijengwa upya na Binui, mwana wa Henadadi. Sehemu inayofuata, tokea pembeni mwa ukuta na mnara wa ikulu ya juu karibu na uwanda wa ulinzi ilijengwa upya na Palali, mwana wa Uzai. Pedaia, mwana wa Paroshi, akishirikiana na watumishi wa hekalu waliokaa Ofeli, walijenga upya sehemu inayokabiliana na Lango la Maji, upande wa mashariki na mnara mrefu. Sehemu nyingine inayofuata, ikitokea kwenye mnara mrefu hadi ukuta wa Ofeli ilijengwa upya na wakazi wa mji wa Tekoa. Juu ya Lango la Farasi palijawa na makuhani, kila mmoja alijenga sehemu inayokabiliana na nyumba yake. Sadoki, mwana wa Imeri alijenga upya sehemu inayokabiliana na nyumba yake. Sehemu inayofuata, ilijengwa upya na Shemaya, mwana wa Shekania, mlinzi wa Lango la Mashariki. Sehemu inayofuata ikiwa ni sehemu yao ya pili ilijengwa upya na Hanania mwana wa Shelemia, akishirikiana na Hanuni, mwana wa sita wa Zalafu. Meshulamu, mwana wa Berekia, alijenga upya sehemu inayokabiliana na chumba chake. Sehemu inayofuata, toka nyumba waliyoitumia wafanyakazi wa hekalu na wafanyabiashara iliyokuwa inaelekeana na Lango la Gereza, karibu na chumba cha juu kwenye pembe upande wa kaskazini-mashariki ilijengwa upya na Malkiya, mfua dhahabu. Sehemu ya mwisho kutoka chumba kwenye pembe hadi Lango la Kondoo ilijengwa upya na wafua dhahabu na wafanyabiashara. Sanbalati aliposikia kuwa tumeanza kazi ya kuujenga upya ukuta, alikasirika sana, akaanza kutukebehi, mbele ya rafiki zake na majeshi ya Wasamaria, akisema, “Hawa Wayahudi wanyonge wanafanya nini? Je, kusudi lao ni kuujenga upya mji? Je, watatoa tambiko? Wanaweza kumaliza kazi kwa siku moja tu? Je, wataweza kufanya mawe yaliyorundikana kwenye takataka na kuteketea, yafae kujengea?” Tobia, Mwamoni, aliyekuwa akisimama karibu naye, alitilia mkazo akisema, “Wanajenga nini? Mbweha akipanda juu yake, atabomoa huo ukuta wao wa mawe!” Ndipo nikamwomba Mungu nikisema, “Ee Mungu wetu, sikia wanavyotukebehi; urudishe dharau yao juu yao wenyewe na uwaache watekwe na kuchukuliwa mateka katika nchi ya kigeni. Kamwe usiwasamehe hatia yao, wala dhambi yao kamwe usiisamehe; kwani wamekukasirisha mbele ya wajenzi.” Lakini tuliendelea na ujenzi wa ukuta mpaka ukafikia nusu yake kwa sababu watu walikuwa wamedhamiria kwa dhati. Lakini Sanbalati, Tobia, Waarabu, Waamoni na Waashdodi waliposikia kuwa ujenzi mpya wa ukuta wa Yerusalemu ulikuwa unasonga mbele na kwamba mapengo katika ukuta yanazibwa barabara, wao walizidi kukasirika. Wakala njama kwa pamoja kuja Yerusalemu kutushambulia na hivyo kuleta mvurugano katika mji huo. Ndipo tulipomwomba Mungu wetu na kuweka ulinzi dhidi yao, mchana na usiku. Watu wa Yuda wakawa wakilalamika wakisema, “Nguvu za vibarua zinapungua na bado kuna takataka nyingi za kubeba. Hatuwezi kuendelea kujenga ukuta.” Nao adui zetu wakawa wanasema, “Hawataweza kujua wala kuona, hadi tutakapofika kwao na kuwaua na kusimamisha kazi.” Wayahudi waliokaa miongoni mwa adui zetu waliposikia maneno yao, walitujia mara kumi wakisema, “Watakuja toka kila mahali wanapokaa na kutushambulia.” Hivyo, kwenye sehemu za chini za ukuta ambazo zilikuwa bado kumalizika, nyuma ya ukuta, katika mahali pa wazi, niliwapanga watu kulingana na jamaa zao wakiwa na mapanga, mikuki na pinde. Nilipoona kuwa watu walikuwa na hofu nikawaambia wakuu, maofisa na watu wote kwa ujumla, “Msiwaogope hata kidogo. Mkumbukeni Bwana aliye Mkuu na wa kutisha, basi piganeni kwa ajili ya ndugu zenu, wana wenu, binti zenu, wake zenu na nyumba zenu.” Maadui waliposikia kwamba njama zao tumezigundua na kuwa Mungu amevuruga njama hizo, ndipo sisi sote tulipourudia ukuta, kila mmoja akaendelea na kazi yake. Tokea siku hiyo na kuendelea, nusu ya watumishi wangu wakawa wanaendelea na ujenzi ambapo nusu nyingine ikawa inashika ulinzi wakiwa na mikuki, ngao, pinde na mavazi ya kukinga kifua. Viongozi wetu wakawa upande wa watu wa Yuda waliokuwa wanaujenga ukuta. Hata wale waliokuwa wanabeba vifaa vya ujenzi waliendelea na kazi huku mkono mmoja ukiwa na vifaa vya ujenzi na mkono mwingine silaha yake. Kila mwashi alikuwa na panga lake limefungwa kiunoni mwake na huku anaendelea kujenga. Na mtu wa kupiga tarumbeta alikuwa karibu nami. Nikawaambia wakuu, maofisa na watu wote kwa ujumla “Kazi ni kubwa, nayo imeenea sehemu kubwa hivi ya kwamba tumetawanyika mno juu ya ukuta kila mmoja yuko mbali na mwenzake. Ukiwa mahali popote unapofanya kazi, mara utakaposikia tarumbeta, kimbilia kwetu. Mungu wetu atatupigania.” Hivyo, tukaendelea kufanya kazi yetu na nusu ya watu wakishika silaha tangu mapambazuko hadi nyota zinapoonekana mbinguni. Wakati huo nikawaambia watu, “Kila mwanamume na mtumishi wake atakaa mjini Yerusalemu usiku, ili tuwe na ulinzi usiku, na wakati wa mchana wataendelea na kazi.” Hivyo ikawa mimi, ndugu zangu, watumishi wangu hata na walinzi waliofuatana nami, hatukuvua mavazi yetu; kila mmoja wetu akawa daima na silaha yake mkononi. Baada ya muda kulitokea malalamiko miongoni mwa watu, wanaume kwa wanawake, wakiwalalamikia ndugu zao Wayahudi. Kulitokea waliosema, “Tafadhali tupatie nafaka tule ili tuweze kuishi kwa kuwa sisi, wana wetu na binti zetu tu wengi.” Na wengine wakalalamika, “Tumeweka rehani mashamba yetu, mizabibu yetu hata na nyumba zetu ili kupata nafaka kwa sababu ya njaa.” Tena kukawa na hata wale, waliolalamika, wakisema, “Ili kulipa kodi ya mfalme juu ya mashamba na mizabibu yetu, ilitubidi tukope fedha. Lakini sisi ni sawa na Wayahudi wengine; watoto wetu ni sawa na watoto wao. Hata hivyo, tunawalazimisha watoto wetu kuwa watumwa. Baadhi ya binti zetu tayari ni watumwa. Hatuna uwezo wa kuzuia jambo hili kwani mashamba yetu na mizabibu yetu yameporwa na watu wengine.” Niliposikia malalamiko yao, nilikasirika sana. Nikaamua kuchukua hatua. Nikawashutumu wakuu na maofisa, nikawaambia, “Mnawatoza riba ndugu zenu.” Nikasema, “Kulingana na uwezo tulio nao, tumekuwa tukiwanunua tena ndugu zetu Wayahudi waliokuwa wameuzwa kwa watu wa mataifa mengine. Lakini sasa hata mnawauza ndugu zenu, nasi tunalazimika kuwanunua!” Basi walinyamaza kimya, bila kuwa na la kujibu. Kisha nikawaambia, “Mnalolifanya ni baya. Je, haiwapasi kumcha Mungu wetu ili kuzuia mataifa mengine yaliyo adui zetu yasitusute? Zaidi ya hayo, mimi mwenyewe, ndugu zangu na watumishi wangu tumewaazima ndugu zetu fedha na nafaka. Na hatutadai riba yoyote. Leo hii na muwarudishie mashamba yao, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na nyumba zao, hata na riba ya fedha, nafaka, divai, na mafuta ambayo nilikuwa ninawatoza.” Wao wakaitikia na kusema, “Tutawarudishia na hatutawadai chochote. Tutafanya kama ulivyosema.” Nikawaita makuhani mbele, na viongozi wote wakaapa mbele ya makuhani kufanya kama walivyoahidi. Nilikunguta kibindo changu na kusema, “Kila mmoja asiyetimiza ahadi hii Mungu na amkungute, amtoe katika nyumba yake na katika kazi yake. Basi, akungutike na kubaki mikono mitupu.” Mkutano mzima ukaitikia, na kusema, “Amina” wakamsifu Mwenyezi-Mungu. Watu wakafanya kama walivyokuwa wameahidi. Tangu wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wa nchi ya Yuda kwa miaka kumi na miwili yaani tangu mwaka wa ishirini mpaka mwaka wa thelathini na mbili wa kutawala kwa mfalme Artashasta, sikula chakula kinachostahili kuliwa na mtawala, wala ndugu zangu hawakufanya hivyo. Watawala walionitangulia walikuwa mzigo mzito kwa watu wakiwadai chakula na divai, mbali na kuwadai kuwalipa sarafu za uzito wa shekeli arubaini za fedha. Hata watumishi wao waliwadhulumu watu. Bali, mimi sikufanya hivyo, kwani nilimcha Mungu. Nilikuwa na juhudi nyingi katika ujenzi mpya wa ukuta huu na kamwe sikujipatia hata shamba. Hata watumishi wangu wote walifanya kazi hii kwa bidii. Zaidi ya hayo, kila siku niliwalisha watu 150, wakiwamo Wayahudi na maofisa, mbali na wale watu waliotujia toka mataifa jirani. Kila siku, ili kuwalisha watu hao, nilichinjiwa dume mmoja na kondoo safi sita na kuku. Kila baada ya siku kumi nilitoa kwa wingi viriba vya divai. Lakini licha ya haya yote, kwa kuwa watu walikuwa na mzigo mzito wa kubeba kila siku, sikutaka posho ya ziada. Sasa, ee Mungu wangu, kumbuka wema wangu wote niliowatendea watu hawa. Kisha Sanbalati, Tobia, Geshemu, Mwarabu na adui zetu wengine, waliposikia kuwa tumemaliza ujenzi wa ukuta na kwamba hakuna mapengo yoyote (ingawa tulikuwa bado hatujaweka milango ya malango), Sanbalati na Geshemu walituma ujumbe kwangu wakisema, “Na tukutane kwenye kijiji kimojawapo cha tambarare ya Ono.” Lakini walikusudia kunidhuru. Basi, nikawapelekea wajumbe, nikisema, “Kazi ninayoifanya ni muhimu sana. Hivyo siwezi kuja kwenu ili kazi isije ikasimama.” Waliendelea kunitaka niende kwao mara nne, lakini nikawapa jibu lilelile. Mara ya tano, Sanbalati akanitumia barua ya hadhara kwa njia ya mjumbe wake. Na barua yenyewe iliandikwa ifuatavyo: “Kuna habari zilizoenezwa miongoni mwa mataifa jirani, na Geshemu anathibitisha habari hizi, kuwa wewe pamoja na Wayahudi wenzako mnakusudia kuasi. Hii ndiyo sababu mnaujenga upya ukuta. Kulingana na habari hizo, wewe unakusudia kuwa mfalme wao. Ili kuthibitisha wazo lako, umejiwekea manabii mjini Yerusalemu ili watangaze kuwa ‘Kuna mfalme katika nchi ya Yuda’. Taarifa hii ataarifiwa mfalme Artashasta. Hivyo nashauri wewe na mimi tukutane na kuzungumzia jambo hili.” Nami nikampelekea ujumbe: “Hakuna jambo kama hilo. Habari hizo umezibuni wewe mwenyewe.” Walifanya hivyo ili kututisha wakifikiri: “Hawataendelea na kazi, kwa hiyo, hakuna litakalotendeka.” Nikamwomba Mungu wangu nikisema, “Lakini sasa, ee Mungu, nakuomba unipe nguvu.” Nilipokwenda nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya mwana wa Mehetabeli, ambaye hakuruhusiwa kutoka nyumbani, aliniambia, “Twende tukutane katika nyumba ya Mungu na milango yake tuifunge kwa sababu leo usiku wanakuja kukuua.” Lakini mimi nikajiuliza moyoni, “Je, mtu kama mimi, ana haja ya kukimbia? Mtu kama mimi anahitaji kuingia hekaluni kusudi apate kuishi? Kamwe sitaingia hekaluni.” Kwa bahati nzuri, nilingamua kuwa alikuwa hajatumwa na Mungu, bali alikuwa amekodishwa na Tobia na Sanbalati atangaze mabaya dhidi yangu. Alikuwa amekodishwa kunitishia nami nifanye dhambi. Na kwa njia hii wangepata mwanya wa kuniharibia jina langu ili kushusha hadhi yangu. Nikamwomba Mungu nikisema, “Ee Mungu, kumbuka yote waliyotenda Tobia na Sanbalati, hata yule Noadia, nabii mwanamke, na manabii wengine waliotaka kunifanya niogope.” Basi, ukuta ulikamilika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli; nayo ilichukua muda wa siku hamsini na mbili. Maadui zetu katika mataifa jirani, waliposikia kuwa kazi tumeimaliza, waliogopa na kuona aibu sana; kwani walijua hakika kuwa kazi hii ilikamilika kwa msaada wa Mungu wetu. Wakati huu wote, viongozi wa Wayahudi walikuwa wakiandikiana na Tobia. Wengi miongoni mwa Wayahudi walishirikiana naye kutokana na kiapo chao kwani alikuwa mkwe wa Shekania, mwana wa Ara. Zaidi ya yote, Yehohanani, mwanawe, alikuwa amemwoa binti Meshulamu, mwana wa Berekia. Pia wakanisimulia matendo mema ya Tobia, na habari zangu wakawa wanampelekea. Naye akawa ananiandikia barua ili kunitisha. Baada ya ukuta kukamilika, malango yote kuwa tayari, na kuteuliwa kwa walinzi, waimbaji na Walawi, nilimteua ndugu yangu Hanani kuwa mwangalizi wa Yerusalemu akishirikiana na Hanania aliyekuwa mkuu wa ngome katika Yerusalemu; kwa sababu alikuwa mtu wa kutegemewa na anayemcha sana Mungu, hapakuwapo mwingine aliyelingana naye, nikawaagiza, “Malango yasifunguliwe usiku kucha hadi jua linapokuwa limepanda. Kabla hawajaondoka walinzi ni lazima kufunga milango yote kwa makomeo yake. Teueni walinzi miongoni mwa wakazi wa mji wa Yerusalemu, kila mmoja awe mahali pake kukabiliana na nyumba yake.” Mji wa Yerusalemu ulikuwa mpana na mkubwa, lakini wakazi wake walikuwa wachache na nyumba zilikuwa hazijajengwa. Mungu akanipa moyo kuwakusanya viongozi na watu ili kujua koo zao. Nikapata kitabu cha koo za watu waliorudi toka uhamishoni mara ya kwanza, na hawa wafuatao ndio waliokuwa wameorodheshwa ndani yake. Wale waliokuwa uhamishoni kule Babuloni, walirudi mjini Yerusalemu na nchini Yuda, kila mmoja akarudi mjini kwake. Jamaa zao walikuwa wamekaa Babuloni tangu mfalme Nebukadneza alipowahamishia huko wakiwa mateka. Waliporudi waliongozwa na Zerubabeli, Yeshua, Nehemia, Azaria, Raamia, Nahamani, Mordekai, Bilshani, Misperethi, Bigwai, Nehumu na Baana. Ifuatayo ni idadi ya watu wa koo za Israeli waliorudi toka uhamishoni: Watu wa ukoo wa Paroshi: 2,172; wa ukoo wa Shefatia: 372; wa ukoo wa Ara: 652; wa ukoo wa Pahath-moabu, yaani wazawa wa Yeshua na Yoabu: 2,818; wa ukoo wa Elamu: 1,254; wa ukoo wa Zatu: 845; wa ukoo wa Zakai: 760; wa ukoo wa Binui: 648; wa ukoo wa Bebai: 624; wa ukoo wa Azgadi: 2,322; wa ukoo wa Adonikamu: 667; wa ukoo wa Bigwai: 2,067; wa ukoo wa Adini: 655; wa ukoo wa Ateri (ambao pia unaitwa Hezekia): 98; wa ukoo wa Hashumu: 328; wa ukoo wa Bezai: 324; wa ukoo wa Harifu: 112; wa ukoo wa Gibeoni: 95; Watu wa miji ifuatayo pia walirudi: Wa mji wa Bethlehemu na Netofa: 188; wa mji wa Anathothi: 128; wa mji wa Beth-azmawethi: 42; wa miji ya Kiriath-yearimu, Kefira na Beerothi: 743; wa miji ya Rama na Geba: 621; wa mji wa Mikmashi: 122; wa miji ya Betheli na Ai: 123; wa mji mwingine wa Nebo: 52; wa mji mwingine wa Elamu: 1,254; wa mji wa Harimu: 320; wa mji wa Yeriko: 345; wa miji ya Lodi, Hadidi na Ono: 721; wa mji wa Senaa: 3,930. Ifuatayo ni idadi ya makuhani waliorudi kutoka uhamishoni: Makuhani wa ukoo wa Yedaya, waliokuwa wazawa wa Yeshua: 973; wa ukoo wa Imeri: 1,052; wa ukoo wa Pashuri: 1247; wa ukoo wa Harimu: 1017. Walawi wa ukoo wa Yeshua, yaani Kadmieli, wazawa wa Hodavia waliorudi kutoka uhamishoni walikuwa 74. Waimbaji: Wazawa wa Asafu walikuwa 148. Walinzi: Wazawa wa Shalumu, wa Ateri, wa Talmoni, wa Akubu, wa Hatita na wa Shobai, walikuwa 138. Koo za wahudumu hekaluni waliorudi kutoka uhamishoni zilikuwa: Ukoo wa Ziha, wa Hasufa, wa Tabaothi; wa Kerosi, wa Siaha, wa Padoni; wa Lebana, wa Hagaba, wa Shalmai; wa Hanani, wa Gideli, wa Gahari; wa Reaya, wa Resini, wa Nekoda; wa Gazamu, wa Uza, wa Pasea; wa Besai, wa Meunimu, wa Nefushesimu; wa Bakbuki, wa Hakufa, wa Harhuri; wa Baslithi, wa Mehida, wa Harsha; wa Barkosi, wa Sisera, wa Tema; wa Nezia na ukoo wa Hatifa. Koo za wazawa wa watumishi wa mfalme Solomoni waliorudi kutoka uhamishoni zilikuwa: Ukoo wa Sotai, wa Soferethi, wa Perida; wa Yaala, wa Darkoni, wa Gideli; ukoo wa Shefatia, wa Hatili, wa Pokereth-hasebaimu na ukoo wa Amoni. Basi wahudumu wote wa hekalu na wazawa wa watumishi wa Solomoni, waliorudi kutoka uhamishoni, walikuwa 392. Watu wa miji ifuatayo, nao walirudi: Wa Tel-mela, wa Tel-harsha, wa Kerubu, wa Adoni na wa Imeri; ila haikuwezekana kuthibitisha kama walikuwa wazawa wa Waisraeli wazawa wa Delaya, Tobia na wa Nekoda; jumla: Watu 642. Wazawa wa koo zifuatazo za makuhani pia walirudi: Ukoo wa Hobaya, wa Hakozi na wa Barzilai (aliyekuwa ameoa binti za Barzilai, Mgileadi, naye akachukua jina la ukoo huo). Hao walitafuta orodha yao kati ya wengine walioorodheshwa katika kumbukumbu za koo, lakini ukoo wao haukuwemo. Kwa hiyo hawakuruhusiwa kutiwa katika huduma ya ukuhani kwani walihesabiwa kuwa najisi. Mtawala akawaambia kuwa hawaruhusiwi kushiriki chakula kitakatifu sana, mpaka afike kuhani mwenye kauli ya Urimu na Thumimu. Watu wote waliorudi kutoka uhamishoni jumla yao ilikuwa 42,360. Tena kulikuwa na watumishi wanaume na wanawake 7,337, nao walikuwa waimbaji wanaume na wanawake, wote 245. Walikuwa na farasi 736, nyumbu 245, ngamia 435, na punda 6,720. Baadhi ya wakuu wa koo walichangia kazi ya ujenzi. Mtawala wa mkoa alitoa kilo 8 za dhahabu, mabirika 50, mavazi 530. Baadhi ya wakuu wa koo walitoa kilo 168 za dhahabu, na kilo 1,250 za fedha. Matoleo ya watu wengine wote yalikuwa kilo 168 za dhahabu, kilo 140 za fedha na mavazi ya makuhani 67. Basi, makuhani, Walawi, walinzi wa hekalu, waimbaji, baadhi ya watu wengine, watumishi wa hekalu na watu wote wa Israeli, wakaishi katika miji yao. Kisha watu wote, kwa nia moja, wakakusanyika mjini Yerusalemu kwenye uwanja ulio karibu na Lango la Maji. Wakamwambia Ezra, mwandishi, kukileta kitabu cha sheria ya Mose ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa watu wa Israeli. Ezra, ambaye alikuwa kuhani, akaenda na kukileta kitabu cha sheria ya Mose mbele ya mkutano mzima, wanaume kwa wanawake na yeyote aliyeweza kuielewa hiyo sheria aliposikia. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kwanza ya mwezi wa saba. Kisha watu wote wanaume kwa wanawake na yeyote aliyeweza kuelewa, Ezra aliwasomea sheria ya Mose akiwa mbele ya Lango la Maji tangu asubuhi hadi adhuhuri. Watu wote wakatega masikio yao kusikiliza kwa makini kitabu cha sheria. Ezra, mwandishi, alikuwa amesimama kwenye mimbari ya mbao iliyotengenezwa kwa kusudi hilo; na kwenye mkono wake wa kulia walikuwa wamesimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya; na kwenye mkono wake wa kushoto walikuwa wamesimama Pedaya, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadana, Zekaria na Meshulamu. Ezra akasimama kwenye mimbari, mbele ya watu wote, nao wakawa wanamkazia macho yao kwa utulivu mkubwa. Mara tu Ezra alipokifungua kitabu cha sheria, watu wote wakasimama wima. Ezra akamshukuru Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu na watu wote wakaitikia “Amina! Amina!” Huku wakiwa wameinua mikono yao juu. Kisha wakamsujudia Mungu huku nyuso zao zikigusa ardhi. Walawi wafuatao walisaidia kuwaelewesha watu sheria: Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodia, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani na Pelaya; walifanya hivyo kila mmoja akiwa amesimama mahali pake. Wakasoma vizuri toka kitabu cha sheria ya Mungu na kuifafanua na watu wote waliweza kuielewa. Watu waliposikia sheria, waliguswa mioyoni mwao, ndipo wote walipoanza kulia. Hivyo Nehemia aliyekuwa mtawala na Ezra kuhani na mwandishi, pamoja na Walawi waliowafundisha watu waliwaambia watu wote, “Siku hii ni siku takatifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, hivyo msiomboleze wala kulia. Sasa rudini nyumbani mkafanye sherehe, mle vinono na kunywa divai nzuri, lakini kumbukeni kuwapelekea wale ambao hawana cha kutosha; kwani leo ni siku takatifu kwa Bwana wetu. Msihuzunike kwa sababu furaha anayowajalia Mwenyezi-Mungu itawapeni nguvu.” Hivyo, Walawi wakawatuliza watu wote, wakisema, “Tulieni kwani siku ya leo ni takatifu; msihuzunike.” Watu wote wakarudi nyumbani kwao kula na kunywa; wakifurahi na kuwagawia wengine chakula kwa kuwa waliyaelewa yote waliyotangaziwa. Kesho yake, wakuu wa koo pamoja na makuhani na Walawi wakakusanyika kwa Ezra mwandishi, ili kujifunza sheria. Wakagundua kuwa, imeandikwa katika kitabu cha sheria kuwa Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose, kwamba watu wanapaswa kukaa vibandani wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba. Hivyo wakatangaza katika miji yao yote na huko Yerusalemu, wakisema, “Nendeni milimani, mkalete matawi ya mizeituni, mizeituni mwitu, mihadasi, mitende na miti mingineyo ili kujengea vibanda, kama ilivyoandikwa.” Basi, watu wakaenda kuleta matawi, wakajijengea vibanda kila mtu kwenye dari na kwenye baraza ya nyumba yake, kwenye baraza za nyumba ya Mungu, kwenye uwanja wa Lango la Maji na uwanja wa Lango la Efraimu. Watu wote waliorudi kutoka uhamishoni wakatengeneza vibanda wakaishi humo. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza watu kuishi katika vibanda tangu wakati Yeshua, mwana wa Nuni alipokuwa akiishi. Watu walifurahi sana. Kila siku, tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho, Ezra aliwasomea watu kitabu cha sheria ya Mungu. Waliadhimisha sikukuu hiyo kwa muda wa siku saba, na siku ya nane wakafanya mkutano mkubwa wa kufunga sikukuu, kama ilivyoagizwa. Siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wa saba, watu wa Israeli walikusanyika, wakifunga na kuvaa mavazi ya magunia na kujipaka udongo kichwani kuonesha majuto yao. Wakati huo, walikuwa wamejitenga mbali na watu wa mataifa mengine, wakasimama na kuungama dhambi zao na maovu ya babu zao. Kwa muda wa kama masaa matatu, walisimama huku sheria ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, inasomwa. Na kwa masaa matatu yaliyofuata, walikuwa wakitubu na kumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Kuliwekwa jukwaa la Walawi; hapo walisimama Yeshua, Bani, Kadmieli, Shebania, Buni, Sherebia, Bani na Kenani. Wakamwomba kwa sauti kubwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walawi, yaani: Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabuea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakawaambia watu; “Simameni na kumsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Msifuni milele na milele! Na watu walisifu jina lako tukufu, ambalo hutukuka kuliko baraka na sifa zote.” Ezra akaomba kwa sala ifuatayo: “Wewe peke yako ndiwe Mwenyezi-Mungu; ndiwe uliyefanya mbingu na jeshi lake lote, dunia na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo; nawe ndiwe unayevihifadhi hai, na jeshi lote la mbinguni lakuabudu wewe. Wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu uliyemchagua Abramu, ukamtoa toka Uri ya Wakaldayo na kumpa jina Abrahamu. Ukamwona kuwa yu mwadilifu mbele yako; ukafanya agano naye kuwapa wazawa wake nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wayebusi na Wagirgashi. Na ahadi yako ukaitimiza; kwani wewe u mwaminifu. “Uliyaona mateso ya babu zetu walipokuwa nchini Misri, na walipokuomba msaada kwenye Bahari ya Shamu uliwasikia. Ulifanya ishara na maajabu dhidi ya Farao, watumishi wake wote na watu wote wa nchi yake; kwani ulijua kuwa waliwakandamiza babu zetu. Ukajipatia umaarufu uliopo mpaka leo. Uliigawa bahari katikati mbele yao, nao wakapita katikati ya bahari, mahali pakavu. Lakini ukawatupa Wamisri waliowafuatia kama jiwe zito ndani ya maji mengi. Mchana uliwaongoza kwa mnara wa wingu, na usiku uliwaongoza kwa mnara wa moto ili kuwamulikia njia ya kuendea. Kule mlimani Sinai ulishuka toka mbinguni na kuzungumza nao. Ukawapa maagizo safi, sheria za kweli, kanuni nzuri na amri. Kwa njia ya Mose, mtumishi wako, ukawajulisha Sabato yako takatifu na ukawaagiza kuzifuata amri, kanuni na sheria ulizowaamrisha. Walipokuwa na njaa, ukawapa chakula kutoka mbinguni. Walipokuwa na kiu ukawapa maji kutoka kwenye mwamba. Ukawaagiza kuichukua nchi uliyokuwa umewaahidi. Lakini wao na babu zetu wakawa na kiburi na wakawa na shingo ngumu wakakataa kufuata maagizo yako. Wakakataa kutii; wasiyakumbuke maajabu uliyofanya miongoni mwao. Wakawa na shingo zao ngumu, wakajichagulia kiongozi wa kuwarudisha utumwani nchini Misri. Bali wewe Mungu u mwepesi kusamehe, mwenye neema na huruma, wewe hukasiriki upesi. U mwenye fadhili nyingi, na hukuwatupa. Hata walipojitengenezea sanamu ya ndama na kusema, ‘Huyu ndiye mungu wetu aliyetutoa kutoka nchi ya Misri,’ wakawa wamefanya kufuru kubwa. Wewe kwa huruma zako nyingi hukuwatupa kule jangwani. Mnara wa wingu uliowaongoza mchana haukuondoka, wala mnara wa moto uliowamulikia njia usiku, haukuondoka. Ukawapa roho yako njema kuwashauri; ukawapa mana kuwa chakula chao na maji ya kunywa ili kutuliza kiu chao. Ukawatunza jangwani kwa miaka arubaini na hawakukosa chochote; mavazi yao hayakuchakaa wala nyayo zao hazikuvimba. “Ukawaruhusu kushinda falme na mataifa, ukawafanyia mengi kila upande. Wakaishinda nchi ya Heshboni alikotawala mfalme Sihoni; na tena wakaishinda nchi ya Bashani alikotawala mfalme Ogu. Wazawa wao ukawafanya wawe wengi kama nyota za mbinguni; ukawaleta katika nchi uliyowaahidi babu zao. Hivyo, hao wazawa wakaja na kuimiliki nchi; uliwashinda wakazi wa nchi hiyo, Wakanaani, ukawatia mikononi mwao, pamoja na wafalme wao, watu wao na nchi yao ili wawatende wapendavyo. Miji yenye ngome wakaiteka, wakachukua nchi yenye utajiri, majumba yenye vitu vingi vizuri, visima vilivyochimbwa, mashamba ya mizabibu na mizeituni pamoja na miti yenye matunda kwa wingi. Hivyo wakala, wakashiba na kunenepa na kuufurahia wema wako. Lakini hawakuwa waaminifu kwako. Wakakuasi, wakaiacha sheria yako na kuwaua manabii waliowaonya ili wakurudie wewe. Wakakufuru sana. Hivyo, ukawatia katika mikono ya adui zao, nao wakawatesa. Lakini wakiwa katika mateso yao, wakakulilia, nawe ukawasikia kutoka mbinguni. Na kwa huruma zako nyingi, ukawapelekea viongozi wa kuwaokoa; nao wakawakomboa toka mikononi mwao. Lakini amani ilipopatikana wakatenda dhambi tena mbele yako, nawe ukawaacha watiwe katika mikono ya adui zao wawatawale. Hata hivyo, walipotubu na kukulilia ukawasikiliza kutoka mbinguni. Na kwa kulingana na huruma zako nyingi, ukawaokoa mara nyingi. Ukawaonya ili wairudie sheria yako. Hata hivyo, kwa kiburi chao, wakaacha kuzitii amri zako. Wakayaasi maagizo yako, ambayo kwayo mtu akiyatii, ataishi. Wakawa wajeuri pia wakafanya shingo zao ngumu, na wakakataa kuwa watiifu. Ukawavumilia kwa miaka mingi, na kuwaonya kwa njia ya roho yako kwa kupitia manabii wako; hata hivyo hawakusikiliza. Basi ukawaacha ukawatia mikononi mwa mataifa mengine. Hata hivyo, kutokana na huruma zako nyingi, hukuwaacha waangamie kabisa au kuwatupa, kwani wewe u Mungu mwenye neema na huruma. Kwa hiyo, ee Mungu wetu, Mungu Mkuu, mwenye nguvu na wa kutisha, wewe unalishika agano lako na una fadhili nyingi. Mateso yaliyotupata, sisi, wafalme wetu, wakuu wetu, makuhani wetu, manabii wetu, babu zetu na watu wako wote tangu wakati wa wafalme wa Ashuru mpaka leo, usiyaone kuwa ni madogo. Hata hivyo, unayo haki kwa kutuadhibu hivyo; kwani wewe umekuwa mwaminifu ambapo sisi tumekuwa watenda maovu. Wafalme wetu, wakuu wetu, makuhani wetu na babu zetu hawajaishika sheria yako wala kujali amri yako na maonyo yako uliyowapa. Hawakukutumikia katika ufalme wao, wala walipoyafurahia mema yako mengi uliyowajalia kwa wingi, katika nchi kubwa na yenye rutuba uliyowapa hawakuyaacha matendo yao maovu. Na leo tumekuwa watumwa; tu watumwa katika nchi uliyowapa babu zetu wafurahie matunda na vipawa vyake vyema. Kwa sababu ya dhambi zetu, utajiri wa nchi hii unawaendea wafalme uliowaleta kututawala. Wanatutawala wapendavyo hata na mifugo yetu wanaitendea wapendavyo, tumo katika dhiki kuu.” Kutokana na haya yote yaliyotokea, sisi tunaweka agano imara na wakuu wetu kwa maandishi; Walawi na makuhani wanatia sahihi zao na mhuri wao. Kwenye hati yenye mhuri kulikuwapo majina ya Nehemia, mtawala wa mkoa, mwana wa Hakalia, na Sedekia; Seraya, Azaria, Yeremia, Pashuri, Amaria, Malkiya, Hatushi, Shebania, Maluki, Harimu, Meremothi, Obadia, Danieli, Ginethoni, Baruku, Meshulamu, Abiya, Miyamini, Maazia, Bilgai na Shemaya. Pia majina ya Walawi: Yeshua, mwana wa Azania, Binui, wazawa wa Henadadi, Kadmieli. Na ndugu zao waliotia sahihi ni: Shebania, Hodia, Kelita, Pelaya, Hanani, Mika, Rehobu, Hashabia, Zakuri, Sherebia, Shebania, Hodia, Bani na Beninu. Majina ya viongozi wa watu: Paroshi, Pahath-moabu, Elamu, Zatu, Bani, Buni, Azgadi, Bebai, Adoniya, Bigwai, Adini, Ateri, Hezekia, Azuri, Hodia, Hashumu, Bezai, Harifu, Anathothi, Nebai, Magpiashi, Meshulamu, Heziri, Meshezabeli, Sadoki, Yadua, Pelatia, Hanani, Anaya, Hoshea, Hanania, Hashubu, Haloheshi, Pilha, Shobeki, Rehumu, Hashabna, Maaseya, Ahia, Hanani, Anani, Maluki, Harimu na Baana. Sisi sote watu wa Israeli, makuhani, Walawi, wangoja malango, waimbaji, watumishi wa hekalu na watu wote waliojitenga na mataifa jirani kufuata sheria ya Mungu pamoja na wake zao, wana wao na binti zao, wote wenye maarifa na fahamu, tunaungana na ndugu zetu, wakuu wetu, katika kula kiapo na kwamba tukivunja kiapo hiki tutaapizwa, na twaapa kuwa tutaishi kwa kufuata sheria ya Mungu ambayo aliitoa kwa njia ya Mose, mtumishi wake. Tena tutatii yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, anatuamuru, na kuwa tutashika maagizo yake na kufuata masharti yake. Binti zetu hatutawaoza kwa watu wa nchi hii na wala wana wetu hawataoa kwao. Ikiwa watu hao wanaleta bidhaa au nafaka kuuza siku ya Sabato, sisi hatutanunua siku hiyo wala siku nyingine yoyote iliyo takatifu. Mwaka wa saba hatutailima ardhi na madeni yote tutayafuta. Tunajiwekea sheria kwamba kwa mwaka tutatoa theluthi moja ya shekeli kwa ajili ya gharama za huduma ya nyumba ya Mungu: Mikate mitakatifu, sadaka za nafaka za kawaida, sadaka za kuteketezwa za kawaida, sadaka za siku za Sabato, sikukuu za mwandamo wa mwezi, sikukuu nyingine zilizowekwa, vitu vingine vitakatifu, sadaka za kuondoa dhambi, ili kuwafanyia upatanisho watu wa Israeli na kazi nyingine zozote za nyumba ya Mungu wetu. Sisi sote, watu wote, makuhani na Walawi tutapiga kura kila mwaka ili kuchagua ukoo utakaoleta kuni za kuteketeza tambiko madhabahuni pa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama sheria ilivyo. Tunaahidi kuleta kila mwaka malimbuko yetu ya mazao na ya matunda ya kila mti kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kwa kufuata ilivyoandikwa katika sheria kila mzaliwa wa kwanza wa kiume, katika nyumba zetu, atapelekwa katika nyumba ya Mungu wetu kwa makuhani wanaohudumu humo, pia tutapeleka kila mtoto wa kwanza wa kiume wa ng'ombe wetu, mbuzi wetu na kondoo wetu. Kila unga wetu wa kwanza, matoleo yetu, matunda ya miti, divai na mafuta tutavileta kwa kuhani kwenye vyumba vya nyumba ya Mungu wetu. Tena tutaleta zaka zetu za mazao yetu kwa Walawi, kwani ndio wanaohusika na ukusanyaji wa zaka hizo katika vijiji vyetu. Kuhani, mzawa wa Aroni, atakuwa na Walawi wanapopokea zaka. Halafu Walawi watapeleka sehemu ya kumi ya zaka zote zilizotolewa katika nyumba ya Mungu kwenye vyumba na ghala. Watu wa Israeli na Walawi watayapeleka matoleo ya nafaka, divai na mafuta ya zeituni kwenye vyumba ambamo vyombo vya patakatifu vinatunzwa na ambamo makuhani, wangoja malango na waimbaji wana vyumba vyao. Na daima tutaijali nyumba ya Mungu wetu. Kisha, viongozi wa watu wakakaa mjini Yerusalemu; watu wengine wote, wakapiga kura kati ya kila jamaa kumi ili kuchagua jamaa moja itakayokaa mjini Yerusalemu, mji mtakatifu. Jamaa nyingine tisa zikakaa katika miji yao mingine. Watu wakawasifu wale wote waliokubali kukaa mjini Yerusalemu. Na katika miji mingine, watu wa Israeli, makuhani, Walawi, walinzi wa malango na wazawa wa watumishi wa Solomoni, walikaa katika maeneo yao wenyewe, katika miji yao. Baadhi ya watu wa kabila la Yuda na wa kabila la Benyamini walikaa katika mji wa Yerusalemu. Wafuatao ndio watu wa ukoo wa Yuda waliokaa mjini Yerusalemu: Athaya, mwana wa Uzia, mwana wa Zekaria, mwana wa Amaria, mwana wa Shefatia, mwana wa Mahalaleli. Wote hao ni wazawa wa Peresi. Pia Maaseya, mwana wa Baruku, mwana wa Kolhoze, mwana wa Hazaya, mwana wa Adaya, mwana wa Yoyaribu, mwana wa Zekaria, Mshilo. Wazawa wote wa Peresi waliokaa mjini Yerusalemu walikuwa wanaume mashujaa 468. Watu wa ukoo wa Benyamini waliokaa mjini Yerusalemu ni: Salu, mwana wa Meshulamu, mwana wa Yoedi, mwana wa Pedaya, mwana wa Kolaya, mwana wa Maaseya, mwana wa Ithieli na mwana wa Yeshaya. Baada ya huyo walikuwako Gabai na Salai. Jumla yao 928. Yoeli, mwana wa Zikri, alikuwa ndiye mkuu wao; naye Yuda mwana wa Hasenua alikuwa mkuu wa pili wa mji. Makuhani waliokaa mjini Yerusalemu walikuwa: Yedaya, mwana wa Yoaribu, Yakini, Seraya, mwana wa Hilkia, mwana wa Meshulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayothi, mwana wa Ahitubu aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya Mungu; hao pamoja na ndugu zao waliofanya kazi hekaluni; walikuwa watu 822. Pamoja na hao, kulikuwa na Adaya, mwana wa Yerohamu, mwana wa Pelalia, mwana wa Amsi, mwana wa Zekaria, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkiya; pia kulikuwa ndugu zake waliokuwa wakuu wa jamaa za baba zao; wote pamoja walikuwa watu 242. Pia walikuwako Amaasai, mwana wa Azareli, mwana wa Ahzai, mwana wa Meshilemothi, mwana wa Imeri, pamoja na ndugu zao; wote wakiwa 128, watu mashujaa. Na mkuu wao alikuwa Zabdieli mwana wa Hagedolimu. Nao Walawi waliokaa mjini Yerusalemu walikuwa: Shemaya, mwana wa Hashubu, mwana wa Azrikamu, mwana wa Hashabia, na mwana wa Buni. Shabethai na Yozabadi, wakuu wa ukoo wa Walawi, walikuwa wasimamizi wa kazi za nje ya nyumba ya Mungu, na Matania, mwana wa Mika, mwana wa Zabdi, mzawa wa Asafu, aliyekuwa kiongozi wakati wa kuomba sala za shukrani. Bakbukia alikuwa msaidizi wake. Pamoja nao alikuwako Abda, mwana wa Shamua, mwana wa Galali na mzawa wa Yeduthuni. Walawi wote waliokaa mjini Yerusalemu, mji mtakatifu, walikuwa 284. Wangoja malango waliokaa mjini Yerusalemu walikuwa: Akubu na Talmoni pamoja na ndugu zao waliokuwa wakilinda malango, walikuwa 172. Watu wengine wa Israeli, makuhani na Walawi walikaa katika miji ya Yuda, kila mmoja katika urithi wake. Lakini watumishi wa hekalu walikaa mjini Yerusalemu katika eneo la Ofeli wakiwa chini ya usimamizi wa Ziha na Gishpa. Kiongozi wa Walawi waliokaa mjini Yerusalemu alikuwa, Uzi, mwana wa Bani, mwana wa Hashabia, mwana wa Matania, mwana wa Mika wa ukoo wa Asafu, waliokuwa waimbaji, viongozi waangalizi wa shughuli za nyumba ya Mungu. Mfalme alikuwa ametoa amri kuhusu zamu zao na mahitaji yao ya kila siku. Pethahia, mwana wa Meshezabeli, wa ukoo wa Zera katika kabila la Yuda, alikuwa mwakilishi kwa mfalme kuhusu mambo yote ya watu wa Yuda. Watu wengine walikaa katika miji karibu na mashamba yao. Baadhi ya watu wa kabila la Yuda walikaa Kiriath-arba, Diboni na Yekabzeeli pamoja na vijiji vilivyoizunguka. Wengine pia walikaa katika miji ya Yeshua, Molada, Beth-peleti, Hasar-shuali na Beer-sheba pamoja na vijiji vilivyoizunguka. Wengine walikaa katika mji wa Ziklagi, Mekona na vijiji vilivyoizunguka. Wengine walikaa katika miji ya Enrimoni, Sora, Yarmuthi, Zanoa na Adulamu pamoja na vijiji vilivyoizunguka, Lakishi na mashamba yaliyouzunguka, na katika Azeka pamoja na vijiji vilivyouzunguka. Hii ina maana kwamba watu wa Yuda walikaa katika eneo lililoko kati ya Beer-sheba upande wa kusini na Bonde la Hinomu upande wa kaskazini. Watu wa kabila la Benyamini walikaa Geba, Mikmashi, Ai, Betheli na vijiji vinavyoizunguka. Wengine walikaa Anathothi, Nobu, Anania, Hazori, Rama, Gitaimu, Hadidi, Seboimu, Nebalati, Lodi na Ono lililokuwa Bonde la Mafundi. Baadhi ya Walawi wa Yuda walichanganyikana na watu wa Benyamini. Ifuatayo ni orodha ya makuhani na Walawi waliorudi kutoka uhamishoni pamoja na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na kuhani mkuu Yeshua. Makuhani: Seraya, Yeremia, Ezra, Amaria, Maluki, Hatushi, Shekania, Rehumu, Meremothi, Ido, Ginethoni, Abiya, Miyamini, Maadia, Bilga, Shemaya, Yoyaribu, Yedaya, Salu, Amoki, Hilkia na Yedaya. Hao walikuwa ni wakuu wa makuhani na ndugu zao wakati wa Yeshua. Walawi: Yeshua, Binui, Kadmieli, Sherebia, Yuda na Matania, ambaye alihusika na usimamizi wa nyimbo za shukrani akishirikiana na ndugu zake. Nao Bakbukia na Uno rafiki zao, walisimama ibadani mkabala nao. Yeshua alimzaa Yoyakimu, Yoyakimu alimzaa Eliashibu, Eliashibu alimzaa Yoyada, Yoyada alimzaa Yonathani na Yonathani akamzaa Yadua. Yoyakimu alipokuwa kuhani mkuu, makuhani wafuatao walikuwa wakuu wa koo zao: Wa Seraya, Meraya; wa Yeremia, Hanania; wa Ezra, Mehulamu; wa Amaria, Yehohanani; wa Maluki, Yonathani; wa Shebania, Yosefu; wa Harimu, Adna; wa Merayothi, Helkai; wa Ido, Zekaria; wa Ginethoni, Meshulamu; wa Abiya, Zikri; ukoo wa Miniamini; wa Moadia, Piltai; wa Bilga, Shamua; wa Shemaya, Yehonathani; wa Yoaribu, Matenai; wa Yedaya, Uzi; wa Salai, Kalai; wa Amoki, Eberi; wa Hilkia, Heshabia; na wa ukoo wa Yedaya, Nethaneli. Wakati wa Eliashibu, Yoyada, Yohanani na Yadua wakuu wa jamaa za Walawi, waliorodheshwa; vilevile wakati wa utawala wa mfalme Dario wakuu wa jamaa za makuhani waliorodheshwa. Wakuu wa jamaa za ukoo wa Lawi waliorodheshwa katika kitabu cha Kumbukumbu mpaka wakati wa Yohanani mjukuu wa Eliashibu. Viongozi wa Walawi: Hashabia, Sherebia, Yeshua mwana wa Kadmieli walisimama mkabala na ndugu zao; walipangwa kuimba nyimbo za kusifu na kushukuru, kufuatana na amri ya mfalme Daudi, mtu wa Mungu. Mabawabu walikuwa: Matania, Bakbukia, Obadia, Meshulamu, Talmoni na Akubu; pia hao walikuwa walinzi wa ghala. Watu hao waliishi wakati wa Yoyakimu, mwana wa Yeshua mwana wa Yosadaki na pia wakati wa Nehemia aliyekuwa mtawala wa mkoa; na hata wakati wa Ezra kuhani na mwandishi. Kisha wakati wa kuweka wakfu ukuta wa Yerusalemu Walawi walitafutwa kila mahali walipokaa ili kuja Yerusalemu kusherehekea kwa furaha pamoja na shukrani na nyimbo, wakitumia matoazi, vinubi na zeze. Wazawa wa waimbaji wakakusanyika kutoka viunga vya Yerusalemu na vijiji vya Wanetofathi, pia kutoka Beth-gilgali, eneo la Geba na Azmawethi, kwa sababu waimbaji walikuwa wamejijengea vijiji kandokando ya Yerusalemu. Makuhani na Walawi walijitakasa, pia waliwatakasa watu, malango na ukuta. Niliwakusanya viongozi wote wa Yuda kwenye ukuta na kutenga waimbaji katika makundi mawili makubwa yaliyoimba nyimbo za shukrani wakiwa katika maandamano. Kundi moja lilielekea upande wa kulia wa ukuta hadi kwenye Lango la Takataka. Waimbaji hao walifuatiwa na Hoshaya akiwa pamoja na nusu ya viongozi wa Yuda. Pamoja naye walikwenda Azaria, Ezra, Meshulamu, Yuda, Benyamini, Shemaya na Yeremia. Wazawa wafuatao wa makuhani walikuwa na tarumbeta: Zekaria, mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya aliyekuwa mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu. Ndugu zake wafuatao waliimba kwa ala za muziki za mfalme Daudi, mtu wa Mungu, yaani Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda na Hanani, walitanguliwa na Ezra mwandishi. Kwenye Lango la Chemchemi walipanda ngazi kuelekea mji wa Daudi, wakaipita Ikulu ya Daudi, na kuelekea nyuma kwenye ukuta hadi kwenye Lango la Maji, mashariki ya mji. Kundi lingine lililoimba nyimbo za shukrani lilielekea upande wa kushoto juu ya ukuta. Mimi nilifuatana na kundi hili pamoja na nusu ya watu. Tulipitia Mnara wa Tanuri hadi kwenye Ukuta Mpana. Na kutoka hapo, tulipitia Lango la Efraimu, Lango la Yeshana, Lango la Samaki, Mnara wa Hananeli, Mnara wa Mia Moja mpaka kwenye Lango la Kondoo. Tulimalizia maandamano yetu kwenye Lango la Gereza. Hivyo, makundi yote mawili yaliyokuwa yanaimba nyimbo za shukrani yalisimama katika nyumba ya Mungu, pamoja nami na nusu ya viongozi; hata na makuhani waliokuwa na tarumbeta: Eliakimu, Maaseya, Miniamini, Mikaya, Eliehoenai, Zekaria na Hanania. Hao walifuatwa na Maaseya, Shemaya, Eleazari, Uzi, Yehohanani, Malkiya, Elamu na Ezeri. Waimbaji waliimba wakiongozwa na Yezrahia. Siku hiyo, watu walitoa tambiko nyingi na kufurahi kwani Mungu aliwafanya wawe na furaha kubwa. Pia wanawake na watoto, wote walifurahi. Vigelegele vya furaha toka mjini Yerusalemu vilisikika mbali. Wakati huo walichaguliwa watu wa kutunza vyumba vya ghala ambamo matoleo kwa ajili ya hekalu yalitunzwa, malimbuko ya kwanza, zaka na kuyakusanya kutoka mashamba ya miji, kwa ajili ya makuhani na Walawi kama ilivyotakiwa na sheria. Watu wote waliwafurahia makuhani na Walawi waliohudumu, kwa sababu walifanya ibada ya Mungu wao na ibada ya utakaso, kama waimbaji walivyoimba hata walinzi wa malango kulingana na agizo la mfalme Daudi na Mfalme Solomoni mwanawe. Tangu wakati wa mfalme Daudi na Asafu kulikuweko kiongozi wa waimbaji, na kulikuwako nyimbo za sifa na shukrani kwa Mungu. Watu wote wa Israeli, tangu wakati wa Zerubabeli na Nehemia, walitoa matoleo ya kila siku ambayo yaliwatunza waimbaji walinda malango. Zaidi ya yote, watu wa Israeli walitoa matoleo kwa ajili ya Walawi, nao Walawi wakatenga sehemu kwa ajili ya wazawa wa Aroni. Katika siku hiyo ya sherehe, kitabu cha Mose kilisomwa na ilifahamika kuwa Waamoni na Wamoabu kamwe wasiingie katika mkutano wa watu wa Mungu. Maana watu wa Israeli, walipokuwa wanasafiri toka Misri, hawakuwapa chakula wala maji ya kunywa, badala yake walimkodisha Balaamu kuwalaani watu wa Israeli, lakini Mungu wetu aligeuza laana yao kuwa baraka. Watu wa Israeli waliposikia sheria hiyo waliwatenga watu wa mataifa mengine. Kabla ya siku ya sherehe, kuhani Eliashibu aliyekuwa ameteuliwa kuangalia vyumba vya nyumba ya Mungu wetu, na mwenye uhusiano mwema na Tobia, alimruhusu Tobia kutumia chumba kikubwa ambamo hapo awali walikuwa wameweka tambiko za nafaka, ubani, vyombo, zaka za nafaka, divai, mafuta; vitu hivyo vyote Waisraeli walivyoagizwa kuwapa Walawi, waimbaji, walinda malango, na matoleo kwa makuhani. Wakati mambo haya yalipokuwa yanatendeka mimi sikuwako Yerusalemu; kwani katika mwaka wa thelathini na mbili wa utawala wa mfalme Artashasta wa Babuloni, nilikuwa nimeomba likizo; nami nikaenda kutoa ripoti kwake. Niliporudi Yerusalemu ndipo nikagundua uovu wa Eliashibu wa kumpa Tobia chumba katika ua wa nyumba ya Mungu. Nilikasirika sana na nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia. Niliamuru watu, nao wakatakasa vyombo hivyo, ndipo nikarudisha humo vifaa vya nyumba ya Mungu, pamoja na tambiko za nafaka na ubani. Tena nikagundua kuwa Walawi hawakupewa haki zao; na matokeo yake ni kwamba Walawi na waimbaji waliokuwa wakifanya kazi hapo awali, sasa walikwisha rudia mashamba yao. Nikawakemea viongozi, nikasema, “Kwa nini nyumba ya Mungu imeachwa?” Niliwakusanya pamoja na kuwarudisha kazini. Kisha, watu wote wa Israeli, wakaanza tena kuleta zaka zao za nafaka, divai na mafuta kwenye ghala. Nikawateua watu wafuatao kuwa watunzaji wa ghala: Kuhani Shelemia, mwandishi Sadoki na Pedaia Mlawi. Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania akawa msaidizi wao. Walikuwa waaminifu na kazi yao ilikuwa kuwagawia ndugu zao mahitaji yao. Ee, Mungu wangu, nikumbuke kwa ajili ya haya yote na usiyasahau matendo yangu mema niliyofanya kwa ajili ya nyumba yako na kwa ajili ya huduma yako. Wakati huohuo, nikawaona watu wa Yuda wakisindika na kukamua zabibu siku za Sabato. Tena wengine walikuwa wakiwabebesha punda wao nafaka, divai, zabibu, tini na vitu vingine wakivipeleka mjini Yerusalemu. Nikawaonya kuwa hawana ruhusa kuuza vitu siku hiyo. Watu wengine toka mji wa Tiro walileta samaki na bidhaa nyingine mjini Yerusalemu na kuwauzia watu wetu siku ya Sabato. Nikawakemea viongozi wa watu wa Yuda, nikisema, “Uovu gani huu mnaofanya, kuikufuru Sabato? Je, babu zetu hawakufanya uovu wa namna hii hii na kumfanya Mungu wetu kutuletea maafa pamoja na mji huu? Na bado mnaleta ghadhabu yake juu ya watu wa Israeli kwa kuikufuru Sabato.” Hivyo, niliamuru kuwa malango ya mji wa Yerusalemu yafungwe mara Sabato inapoanza jioni, wakati giza linapoanza kuingia, na yasifunguliwe mpaka Sabato imekwisha. Niliweka baadhi ya watumishi wangu kwenye malango na kuwaagiza kuwa kitu chochote kisiletwe mjini siku ya Sabato. Mara mbili au tatu hivi wafanyabiashara waliokuwa wakiuza bidhaa za aina mbalimbali iliwabidi kulala nje ya mji. Niliwaonya na kuwaambia: “Hakuna maana kulala nje ya mji. Mkijaribu tena nitatumia nguvu.” Hivyo tangu wakati huo hawakurudi tena siku ya Sabato. Niliagiza Walawi kujitakasa na kwenda kuyalinda malango ili kutunza Sabato iwe takatifu. Ee, Mungu wangu, nikumbuke hata na kwa hili pia na unihurumie kutokana na fadhili zako kuu. Tena wakati huo niliona Wayahudi waliooa wanawake kutoka Ashdodi, Amoni na Moabu; na nusu ya watoto wao walizungumza Kiashdodi au lugha nyingine na hawakuweza kuzungumza lugha ya Yuda. Niliwakemea na kuwaapiza, hata nikawapiga baadhi yao na kuwavuta nywele zao. Niliwalazimisha kuapa kwa jina la Mungu, nikisema, “Binti zenu msiwaoze kwa vijana wao, wala binti zao wasiolewe na vijana wenu au na nyinyi wenyewe. Je, Solomoni hakutenda dhambi kwa sababu ya wanawake wa namna hiyo? Yeye alikuwa mfalme mkuu kuliko wafalme wa mataifa mengine. Mungu alimpenda na akamfanya kuwa mfalme juu ya watu wote wa Israeli, hata hivyo wanawake wa mataifa mengine, walimfanya hata yeye atende dhambi. Je, sasa tufuate mfano wenu na tutende dhambi hii kubwa ya kutomtii Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni?” Mmoja kati ya wana wa Yoyada, mwana wa kuhani mkuu Eliashibu, alioa binti Sanbalati kutoka mji wa Beth-horoni; kwa sababu hiyo nilimfukuza kutoka mbele yangu. Ee Mungu, kumbuka jinsi watu walivyochafua ukuhani na agano la kikuhani na la Walawi. Niliwatakasa watu kutokana na chochote kilichokuwa cha kigeni. Nikatayarisha mwongozo kwa ajili ya makuhani na Walawi kuhusu kazi ya kila mmoja wao. Niliagiza matoleo ya kuni kufanyika katika wakati unaopaswa na malimbuko wakati wake. Ee Mungu wangu, nikumbuke kwa ajili ya haya yote na unijalie mema. Mfalme Ahasuero, alipotawala ufalme wake ulikuwa mikoa 127, toka India hadi Kushi. Kiti chake cha enzi kilikuwa katika mji mkuu Susa. Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wake, mfalme Ahasuero aliwaandalia karamu viongozi na watumishi wake wa serikali, wakuu wa majeshi ya Persia na Media, watu maarufu na wakuu wa mikoa. Basi, kwa muda wa miezi sita, Ahasuero akaonesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na fahari ya utawala wake. Muda huo ulipomalizika, mfalme aliwaandalia karamu watu wote wa mji mkuu wa Susa, wakubwa kwa wadogo. Karamu hiyo iliyochukua muda wa siku saba, ilifanyika uani, katika bustani ya ikulu. Mahali hapo palikuwa pamepambwa kwa mapazia ya pamba ya rangi nyeupe na vitambaa vya rangi ya buluu. Mapazia hayo yalikuwa yamefungiwa pete za fedha kwa kamba za kitani safi za zambarau, na kuninginizwa kwenye nguzo za marumaru. Makochi ya dhahabu na fedha yalikuwa yamewekwa kwenye sakafu iliyotengenezwa kwa vijiwe vya rangi, marumaru, lulumizi na mawe ya thamani. Watu walipewa vinywaji katika vikombe mbalimbali vya dhahabu, naye mfalme alikuwa mkarimu sana wa divai ya kifalme. Kila mtu alikunywa akashiba; mfalme alikuwa ametoa maagizo kwa watumishi wa ikulu wamhudumie kila mtu kadiri ya mahitaji yake. Wakati huo huo, malkia Vashti naye aliwaandalia akina mama karamu ndani ya ikulu ya Ahasuero. Siku ya saba ya karamu hiyo, mfalme Ahasuero, akiwa amejaa furaha kutokana na divai aliyokuwa amekunywa, aliwaita matowashi saba waliomhudumia yeye binafsi: Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi. Aliwaamuru hao wamlete kwake malkia Vashti, akiwa amevaa taji yake ya kimalkia. Malkia huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, hivyo mfalme alitaka kuwaonesha wageni wake na viongozi uzuri wake. Lakini matowashi hao walipomweleza malkia amri ya mfalme, Vashti alikataa kutii. Jambo hilo lilimwudhi sana mfalme, akawa anawaka hasira moyoni. Ilikuwa desturi ya mfalme kupata mawaidha kutoka kwa wenye hekima, hivyo aliwaita wanasheria na mahakimu ili wamshauri la kufanya. Washauri wake wa kawaida walikuwa Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Maresi, Marsena na Memukani — viongozi saba wa Persia na Media waliokuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake. Aliwauliza hivi: “Je, kulingana na sheria, afanyiwe nini malkia Vashti? Maana, nimewatuma matowashi wangu kwake, lakini yeye amekataa kuitii amri yangu, mimi mfalme Ahasuero!” Hapo Memukani akamwambia mfalme na viongozi wake, “Licha ya kumkosea mfalme, malkia Vashti amewakosea viongozi na kila mtu katika mikoa ya mfalme Ahasuero! Tendo hili la malkia Vashti litajulikana na wanawake wote, nao watawadharau waume zao, wakisema: ‘Mfalme Ahasuero aliamuru malkia Vashti aje kwake, lakini yeye akakataa.’ Leo hii, mabibi wa Persia na Media ambao wamesikia alivyofanya malkia Vashti, watakuwa wanawaeleza viongozi wako; hivyo dharau na chuki vitajaa kila mahali. Basi, ukipenda, ewe mfalme, toa amri rasmi Vashti asije tena mbele yako. Amri hiyo na iandikwe katika sheria za Persia na Media, ili isiweze kubadilishwa. Kisha, cheo chake cha umalkia, apewe mwanamke mwingine anayestahili zaidi yake. Amri hiyo itakapotangazwa katika eneo lote la utawala wako, kila mwanamke atamheshimu mume wake, awe tajiri au maskini.” Wazo hilo lilimpendeza sana mfalme na viongozi wake, akatekeleza kama alivyopendekeza Memukani. Basi, akapeleka barua kwa kila mkoa kwa lugha na maandishi yanayoeleweka mkoani: Kwamba kila mwanamume awe bwana wa nyumba yake, na kuitangaza habari hii kwa lugha yake. Baadaye, hasira yake ilipokwisha tulia, mfalme Ahasuero alimkumbuka Vashti, akawa anatafakari juu ya ukaidi wake na hatua iliyochukuliwa dhidi yake. Basi, watumishi wake, waliokuwa wanamhudumia yeye binafsi, wakamshauri, “Kuna wasichana wengi wazuri; kwa nini usitafutiwe mmoja? Unaweza kuteua maofisa katika kila mkoa wa utawala wako, na kuwaagiza wawalete wasichana wazuri wote kwenye nyumba ya wanawake hapa Susa, mji mkuu. Halafu wawekwe chini ya uangalizi wa Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wako; na hapo wapewe mafuta na vifaa vingine ili wajirembeshe zaidi. Yule atakayekupendeza zaidi, na afanywe malkia badala ya Vashti.” Mfalme akaona shauri hilo ni jema, akafanya hivyo. Mjini Susa, palikuwa na mtu mmoja Myahudi, jina lake Mordekai, mwana wa Yairi mwana wa Shimei, mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini. Mordekai alikuwa miongoni mwa watu wale waliochukuliwa mateka wakati mfalme Yekonia wa Yuda alipotekwa na mfalme Nebukadneza wa Babuloni. Alikuwa na binamu, Esta, ambaye jina lake la Kiebrania lilikuwa Hadasa. Esta alikuwa msichana mzuri wa sura na umbo. Wazazi wake walipofariki, Mordekai alimchukua Esta, akamlea kama binti yake. Amri ya mfalme ilipotangazwa hadharani, wasichana wengi walipelekwa Susa, mji mkuu, wakawekwa chini ya ulinzi wa Hegai. Esta naye, alipelekwa kwenye ikulu ya mfalme, akawekwa chini ya uangalizi wa Hegai, yule mwangalizi wa wanawake. Hegai alipendezwa na Esta hata kiasi cha kumpendelea. Bila kupoteza wakati, alimpa Esta mafuta na chakula maalumu. Isitoshe, alimhamishia mahali pazuri kabisa katika nyumba hiyo ya wanawake, akamteulia watumwa wa kike saba kutoka ikulu ya mfalme, wamhudumie. Esta alikuwa hajajitambulisha ukoo wala kabila lake, maana Mordekai alikuwa amemwonya asifanye hivyo. Kila siku Mordekai alipitapita mbele ya ua wa nyumba hiyo ya wanawake ili apate kujua hali ya Esta na mambo ambayo yangempata. Kipindi cha hao wasichana kujiremba na kujitia uzuri kilichukua mwaka mmoja: Miezi sita ya kwanza walitumia mafuta ya manemane, na miezi sita ya mwisho walitumia manukato na mafuta mengineyo. Baada ya hapo, kila mwali, peke yake, alipelekwa kwa mfalme Ahasuero. Wakati wa kwenda kwa mfalme, kila mwali alipewa kila alichotaka kuchukua kutoka nyumba ya wanawake kwenda nacho ikulu. Jioni ulikuwa ndio wakati wa kwenda, na kesho yake asubuhi, mwali huyo alipelekwa katika nyumba nyingine ya wanawake, chini ya Shaashgazi, towashi msimamizi wa masuria wa mfalme. Mwali haikumpasa kurudi kwa mfalme, isipokuwa kama mfalme amependezwa naye kiasi cha kuagiza aitwe kwa jina. Wakati uliwadia wa Esta kwenda kwa mfalme. Huyo, binti Abihaili, binamu ya Mordekai, na ambaye alilelewa na Mordekai, hakuomba chochote zaidi ya kile alichopangiwa na Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wa mfalme. Kila mtu aliyemwona Esta, alipendezwa naye. Basi, Esta alipelekwa ikulu kwa mfalme katika mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Ahasuero, mwezi wa kumi uitwao Tebethi. Mfalme alipendezwa zaidi na Esta kuliko alivyopendezwa na wanawake wengine wote. Alipendwa sana kuliko wasichana wengine. Basi, mfalme akamvika taji ya kimalkia kichwani, akamfanya malkia badala ya Vashti. Kisha mfalme akaandaa karamu kubwa kwa heshima ya Esta, akawaalika viongozi na watumishi wote wa serikali yake. Pia, mfalme alitangaza msamaha wa kodi katika mikoa yote, akatoa zawadi nyingi kulingana na hadhi yake ya kifalme. Wasichana walipokusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi penye lango la mfalme. Esta alikuwa bado hajajitambulisha ukoo wala kabila lake kama Mordekai alivyokuwa amemwonya asifanye hivyo; naye Esta alimtii kama alivyokuwa akimtii wakati wa utoto wake, alipolelewa naye. Wakati Mordekai alipokuwa anaketi penye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, wawili baadhi ya matowashi wa mfalme waliokuwa walinzi wa milango ya vyumba vya mfalme, waliudhika kiasi cha kula njama kumuua mfalme Ahasuero. Mordekai aliingamua njama hiyo, akamjulisha malkia Esta, naye Esta akampasha habari mfalme. Uchunguzi ulipofanywa, iligunduliwa kuwa ni kweli; basi, watu hao wawili wakatundikwa kwenye mti wa kuulia. Habari kuhusu tukio hilo iliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme. Baada ya mambo hayo, mfalme Ahasuero alimpandisha cheo Hamani, akawa waziri mkuu. Hamani alikuwa mwanawe Hamedatha, na wa uzao wa Agagi. Mfalme aliamuru maofisa wote wa serikali yake wamtii Hamani kwa kumwinamia na kumsujudia. Lakini Mordekai, hakumwinamia wala kumsujudia. Maofisa kadhaa wa mfalme waliokuwa penye lango la mfalme, wakamwuliza Mordekai, “Mbona wewe waidharau amri ya mfalme?” Kila siku walimshauri aache tabia hiyo, lakini Mordekai hakukubaliana nao. Alikataa kufanya hivyo kwa madai kwamba yeye ni Myahudi na kwa hiyo hawezi kumsujudia Hamani. Basi, wakamwarifu Hamani ili waone kama ataivumilia tabia ya Mordekai. Hamani aliwaka hasira alipojua kwamba Mordekai hamwinamii wala hamsujudii. Tena alipogundua kuwa Mordekai alikuwa Myahudi, aliamua kwamba kumwadhibu peke yake haitoshi. Basi akala njama kuwaangamiza Wayahudi wote, watu wa ukoo wa Mordekai, katika utawala wa mfalme Ahasuero. Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa mfalme Ahasuero, mnamo mwezi wa kwanza uitwao Nisani, Hamani aliagiza kura (yaani Purimu) ifanywe kupata siku na mwezi ambapo angetekeleza njama zake. Basi, kura ikaangukia siku ya kumi na nne ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari. Basi, Hamani akamwambia mfalme: “Wapo watu wa taifa fulani walioko kila mahali katika utawala wako, nao wako katika kila mkoa. Watu hao wana sheria zilizo tofauti kabisa na za watu wengine. Isitoshe, wao hawazitii sheria zako, kwa hiyo haikufaidi chochote kuwavumilia. “Ukipenda, ewe mfalme, amri na itolewe, watu hawa waangamizwe. Nami naahidi, kama utaamuru hivyo, nitatoa kiasi cha kilo 10,000 za fedha ziwekwe katika hazina ya mfalme.” Mfalme akaivua pete yake, ambayo ilitumiwa kupigia mhuri matangazo, akampa adui wa Wayahudi Hamani mwana wa Hamedatha wa uzao wa Agagi. Ndipo mfalme akamwambia Hamani, “Umepewa watu wote na hizo fedha, tumia upendavyo.” Basi, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza, Hamani aliwaita makatibu wote wa mfalme, akawapa tangazo ambalo alitaka litafsiriwe kwa kila lugha na kila namna ya maandishi katika utawala huo, halafu nakala zisambazwe kwa watawala wote, wakuu wa mikoa yote, na viongozi wa makabila — kufuatana na lugha zinazotumika kwao. Tangazo hilo lilitolewa kwa jina la mfalme Ahasuero, na kupigwa mhuri kwa pete yake. Matarishi walizipeleka nyaraka hizo kwa kila mkoa katika utawala huo. Tangazo hilo lilisema kwamba kwa siku moja tu, yaani siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari, Wayahudi wote — vijana kwa wazee, wanawake kwa watoto, wote lazima wauawe, waangamizwe na kufutiliwa mbali, na mali zao zote zichukuliwe. Taarifa hiyo ilitakiwa iandikwe hadharani katika kila mkoa, ili kila mtu ajiandae kwa ajili ya siku hiyo. Kwa amri ya mfalme, tangazo hili lilitolewa katika mji mkuu wa Susa, nao matarishi wakalitangaza katika mikoa yote. Mfalme na Hamani walikaa chini kunywa wakati watu mjini Susa wanafadhaika. Mordekai alipojua yote yaliyotukia, alizirarua nguo zake, akavaa vazi la gunia, na kujitia majivu. Kisha, akapita katikati ya mji akilia kwa sauti ya uchungu. Alikwenda mpaka penye lango la ikulu ya mfalme, lakini hakuweza kuingia kwa sababu hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia ikulu akiwa amevaa vazi la gunia. Katika kila mkoa, mara tu amri ya mfalme ilipotangazwa, msiba mkubwa uliwakumba Wayahudi. Walifunga, wakalia na kuomboleza; na wengi wao walilala katika majivu wakiwa wamevaa magunia. Malkia Esta alipoarifiwa na matowashi na watumwa wa kike wake habari za Mordekai alihuzunika sana. Akampelekea Mordekai nguo za kuvaa badala ya vazi la gunia, lakini Mordekai akazikataa. Basi, akamwita Hathaki, mmoja wa matowashi wa mfalme aliyeteuliwa na mfalme amhudumie Esta, akamtuma kwa Mordekai kuuliza kisa na maana ya tukio hilo. Hathaki alimwendea Mordekai uwanjani, mbele ya lango la ikulu. Mordekai akamsimulia Hathaki yote yaliyokuwa yamempata, na kiasi kamili cha fedha ambayo Hamani alikuwa ameahidi kulipa katika hazina ya mfalme kama Wayahudi wote wangeangamizwa. Alimpa pia nakala moja ya tangazo lililokuwa limetolewa mjini Susa kuhusu kuangamizwa kwa Wayahudi, akamwomba amchukulie Esta, amweleze hali ilivyo, na kumwambia aende kumsihi mfalme na kumwomba awahurumie Wayahudi, watu wake Esta. Hathaki akaenda akamweleza Esta yote aliyosema Mordekai. Naye Esta akamwambia Hathaki arudi akamwambie Mordekai, “Watumishi wote wa mfalme na raia wa mikoa yote wanajua ya kwamba mtu yeyote yule akiingia katika ua wa ndani na kumwona mfalme bila kuitwa, huyo ni lazima auawe. Anayeweza kunusurika ni yule tu ambaye mfalme atamnyoshea fimbo yake ya dhahabu ili kumsalimisha. Kumbe mimi sijaitwa na mfalme, yapata mwezi mzima sasa.” Mordekai alipopata ujumbe wa Esta, mara alimpelekea onyo hili: “Usidhani kwamba kwa kuwa upo ikulu wewe u salama zaidi kuliko Myahudi mwingine yeyote yule. Ukikaa kimya wakati kama huu, msaada utawajia Wayahudi kutoka mahali pengine, nao wataokolewa; lakini wewe utakufa, na jamaa ya baba yako itaangamia. Ni nani ajuaye pengine umefanywa malkia kwa ajili ya wakati kama huu!” Esta alimpelekea Mordekai jibu hili: “Nenda ukawakusanye pamoja Wayahudi wote waliopo mjini Susa. Fungeni, msile wala msinywe kwa siku tatu, usiku na mchana, kwa ajili yangu. Na mimi na watumwa wa kike wangu tutafanya vivyo hivyo. Kisha, nitamwendea mfalme, ingawa ni kinyume cha sheria. Kama ni kuuawa, na niuawe.” Basi, Mordekai akaenda zake na kufanya kama Esta alivyomwambia. Siku ya tatu ya mfungo wake, Esta alivalia mavazi yake ya kimalkia, akaenda akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuelekea ukumbi wa mfalme. Mfalme alikuwamo ndani, amekaa katika kiti chake cha enzi, kuelekea mlango wa nyumba ya mfalme. Mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, alipendezwa naye, akamnyoshea fimbo ya dhahabu aliyokuwa ameshika mkononi mwake. Esta akakaribia, akagusa ncha ya fimbo. Hapo mfalme akauliza, “Unataka nini Esta? Niambie unachotaka, nawe utapata — hata kama ni nusu ya ufalme wangu.” Esta akamjibu, “Ukipenda, ewe mfalme, uje leo pamoja na Hamani, kwenye karamu ninayoandaa kwa ajili yako, mfalme.” Mfalme akatoa amri Hamani aje upesi, kama Esta alivyoomba. Basi, mfalme na Hamani wakaenda kwenye karamu aliyoandaa Esta. Walipokuwa wanakunywa divai, mfalme akamwuliza tena Esta: “Unataka nini? Niambie, nawe utapata. Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme wangu, utapewa.” Esta akamjibu, “Ombi langu ni hili: Kama u radhi, ewe mfalme, kukubali ombi langu, basi, naomba wewe na Hamani mje kesho kwenye karamu nyingine nitakayowaandalieni. Wakati huo nitakujulisha ombi langu.” Hamani alitoka huko karamuni mwenye furaha tele na moyo mkunjufu. Lakini alipomwona Mordekai penye lango la ikulu, hasimami wala hampi heshima, Hamani akawaka hasira. Hata hivyo, alijizuia, akaenda zake nyumbani. Halafu akawaalika nyumbani kwake rafiki zake, na kumwomba Zereshi mkewe ajiunge nao. Ndipo akaanza kuelezea juu ya utajiri aliokuwa nao, wana aliokuwa nao, jinsi mfalme alivyompandisha cheo, na jinsi alivyopewa madaraka zaidi kuliko maofisa wengine wote wa mfalme. Hamani akaendelea kujitapa, “Isitoshe malkia Esta hakumwalika mtu mwingine yeyote pamoja na mfalme isipokuwa mimi tu. Hata kesho pia, ametualika mimi na mfalme. Lakini yote haya hayaniridhishi iwapo nitaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai penye lango la ikulu.” Basi, Zereshi, mkewe, na marafiki zake, wakamshauri hivi: “Kwa nini asitengenezewe mti wa kuulia, wenye urefu wa mita ishirini na mbili? Kesho asubuhi, unaweza kuzungumza na mfalme ili Mordekai auawe juu yake, kisha uende ukale karamu na mfalme kwa furaha.” Wazo hilo lilimfurahisha Hamani, naye akatengeneza mti wa kuulia. Usiku huo, mfalme hakupata usingizi. Basi, akaamuru kitabu cha kumbukumbu za matukio ya kila siku kiletwe, nacho kikasomwa mbele yake. Ikaonekana ilivyoandikwa jinsi Mordekai alivyongamua njama ya kumwua mfalme iliyokuwa imefanywa na Bigthana na Tereshi, wawili kati ya matowashi wa mfalme waliokuwa walinzi wa vyumba vya mfalme. Mfalme akauliza, “Je, tumempa Mordekai heshima au tuzo gani kwa jambo hili?” Watumishi wake wakamjibu, “Hujafanya kitu kwa ajili yake.” Mfalme akauliza, “Kuna ofisa yeyote uani?” Ikawa wakati huo Hamani alikuwa ameingia katika ua wa nje wa ikulu; alikuwa amekuja kwa mfalme kuomba Mordekai auawe kwenye mti wa kuulia ambao alikuwa amekwisha mtayarishia. Basi, watumishi wakamjibu mfalme, “Hamani yuko uani.” Mfalme akasema, “Mkaribishe ndani.” Hamani alipoingia ndani, mfalme akamwuliza, “Je, nimfanyie nini mtu ambaye ningependa sana kumtunukia heshima?” Hamani akafikiria moyoni mwake: “Ni nani huyo ambaye mfalme angependa kumtunukia sana heshima? Bila shaka ni mimi.” Basi, Hamani akamjibu mfalme, “Mtu huyo ambaye mfalme angependa kumtunukia heshima, yafaa watumishi wa mfalme walete mavazi safi ya kitani aliyovaa mfalme na farasi wake mwenyewe, na mmoja wa washauri wako wa kuheshimika, ee mfalme, amvishe mtu huyo mavazi hayo ya kifalme, na kumwongoza mtu huyo akiwa amepanda farasi wako mpaka kwenye uwanja wa mji, huku anatangaza: ‘Hivi ndivyo anavyotendewa mtu ambaye mfalme amependa kumpa heshima.’” Hapo mfalme akamwambia Hamani, “Fanya haraka! Chukua mavazi hayo na farasi, ukamtunukie heshima hii Mordekai, Myahudi ambaye hukaa penye lango la ikulu. Usiache kumfanyia hata jambo moja kati ya hayo uliyoyataja.” Basi, Hamani akachukua mavazi hayo na kumvisha Mordekai, akamtembeza kwenye uwanja wa mji akiwa juu ya farasi wa mfalme, huku anatangaza: “Hivi ndivyo anavyotendewa mtu ambaye mfalme amependa kumpa heshima.” Kisha Mordekai akarudi kwenye lango la ikulu. Lakini Hamani akakimbilia nyumbani kwake, amejaa huzuni na amekifunika kichwa chake kwa aibu. Huko akawasimulia Zereshi, mkewe, na rafiki zake wote mambo yote yaliyompata. Zereshi na hao rafiki zake wakamwambia: “Ikiwa huyu Mordekai, ambaye umeanza kupoteza madaraka yako kwake ni wa kabila la Wayahudi, basi, hutamweza; atakushinda kabisa.” Walipokuwa bado wanaongea hayo, matowashi wa mfalme wakafika hima kumchukua Hamani kwenda kwenye karamu ya Esta. Hivyo mfalme na Hamani wakaenda kula karamu na malkia Esta. Katika siku ya pili, walipokuwa wanakunywa divai, mfalme akamwuliza tena Esta, “Sasa, malkia Esta, unataka nini? Niambie, nawe utapata. Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme wangu, utapewa.” Malkia Esta akamjibu, “Kama nimepata upendeleo kwako, ewe mfalme, na ukiwa radhi kunitimizia ombi langu, haja yangu ni mimi niishi na watu wangu pia. Maana, mimi na watu wangu tumeuzwa tuuawe, kuangamizwa na kufutiliwa mbali. Kama tungeuzwa tu kuwa watumwa na watumwa wa kike, ningekaa kimya, wala nisingekusumbua. Ingawa tutakatiliwa mbali hakuna adui atakayeweza kufidia hasara hii kwa mfalme.” Hapo mfalme Ahasuero akamwuliza malkia Esta, “Ni nani huyo athubutuye kufanya jambo kama hilo? Yuko wapi mtu huyo?” Esta akamjibu, “Adui yetu mkuu na mtesi wetu, ni huyu mwovu Hamani!” Hapo Hamani akashikwa na hofu mbele ya malkia na mfalme. Mfalme akasimama kwa hasira, akatoka chumbani kwenye karamu ya divai na kwenda nje kwenye bustani ya ikulu. Hamani alipoona kwamba mfalme amenuia kumwadhibu, alibaki nyuma kumsihi malkia Esta ayasalimishe maisha yake. Baadaye mfalme alirudi kutoka bustanini, na mara alipoingia chumbani walimokuwa wanakunywa divai, alimkuta Hamani amejitupa karibu na kochi ambamo Esta alikuwa amekaa. Kuona hivyo, mfalme alisema kwa sauti kuu, “Hivi mtu huyu anataka kumshika kwa nguvu malkia mbele yangu, tena ndani ya ikulu?” Mara kabla mfalme hajamaliza kusema, matowashi wakamfunika Hamani uso. Harbona, mmoja wa wale matowashi waliomhudumia mfalme, akasema, “Hamani amethubutu hata kutengeneza mti wa kumwulia Mordekai ambaye aliyaokoa maisha yako, ewe mfalme. Mti huo, wenye urefu wa mita ishirini na mbili, bado uko huko nyumbani kwake.” Hapo mfalme akaamuru, “Mwulie Hamani papo hapo.” Naye, Hamani akauawa hapo kwenye mti wa kuulia aliokuwa amemtayarishia Mordekai. Basi, hasira ya mfalme ikapoa. Siku hiyohiyo, mfalme Ahasuero alimkabidhi malkia Esta mali yote ya Hamani, adui ya Wayahudi. Esta akamjulisha mfalme kwamba Mordekai ni jamaa yake. Basi, tangu wakati huo, Mordekai akaruhusiwa kumwona mfalme. Mfalme akaivua pete yake ya mhuri aliyokuwa amemnyanganya Hamani, akampa Mordekai. Esta naye akampa Mordekai mamlaka juu ya mali ya Hamani. Kisha Esta akazungumza tena na mfalme; akajitupa chini, miguuni pa mfalme, huku analia, akamsihi mfalme aukomeshe mpango mbaya ambao Hamani, wa uzao wa Agagi, alikuwa amepanga dhidi ya Wayahudi. Mfalme akamnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu, naye Esta akasimama na kusema, “Ukipenda, ewe mfalme, na kama unanijali na ukiona inafaa, tafadhali, toa tangazo la kufutilia mbali mipango ambayo Hamani alikuwa ameamuru itekelezwe. Mipango hiyo ni ile ya mwana wa Hamedatha, mzaliwa wa Agagi, aliyopanga ili kuwaangamiza Wayahudi wote katika mikoa yote. Maana, ninawezaje kuvumilia kuona watu wangu wanaangamizwa na jamaa zangu wanauawa?” Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, yule Myahudi, “Tazameni! Nimempa Esta mali yake Hamani, naye wamekwisha mnyonga kwa sababu ya njama zake dhidi ya Wayahudi. Mwaweza kuwaandikia Wayahudi lolote mpendalo. Tena mwaweza kuandika kwa jina langu na kutumia mhuri wa kifalme, kwa sababu tangazo ambalo limetolewa kwa jina la mfalme na kupigwa mhuri wa mfalme, haliwezi kubatilishwa.” Basi, mnamo siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu uitwao Siwani, Mordekai aliwaita makatibu wote wa mfalme, akawaagiza waandike barua kwa Wayahudi na wakuu, watawala na maofisa wa mikoa yote 127, kuanzia India mpaka Kushi. Nyaraka hizo ziliandikwa kwa kila mkoa katika lugha yake na hati yake ya maandishi, hali kadhalika kwa Wayahudi. Mordekai alikuwa ameandika nyaraka hizo kwa jina la mfalme Ahasuero, akazipiga mhuri kwa pete ya mfalme. Na waliozipeleka walikuwa matarishi waliopanda farasi wenye nguvu waendao kasi. Kwa njia ya nyaraka hizi mfalme aliwaruhusu Wayahudi katika kila mji kukusanyika ili kuyalinda maisha yao. Walikuwa na ruhusa ya kuharibu, kuua bila huruma na kuangamiza kundi lolote la watu au mkoa, lenye kuwashambulia kwa silaha pamoja na wanawake na watoto wao, na kuziteka nyara mali zao. Jambo hili lingefanyika katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero, mnamo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari. Nakala za tangazo hili ambalo lilitolewa kama sheria katika kila mkoa zilisambazwa kwa kila mtu katika kila mkoa, ili Wayahudi wajiandae kulipiza kisasi siku hiyo ifikapo. Kwa amri ya mfalme, matarishi waliopanda farasi wenye nguvu waendao kasi, waliondoka mbio. Tangazo hili pia lilitolewa katika mji mkuu, Susa. Mordekai alipotoka ikulu kwa mfalme, akiwa amevalia mavazi ya kifalme ya rangi ya urujuani na nyeupe, joho la kitani safi la rangi ya zambarau, na taji kubwa ya dhahabu, mji wa Susa ulijaa shangwe na vigelegele. Hapo Wayahudi waliona fahari, heshima na furaha, wakajisikia wenye nafuu na ushindi. Katika kila mkoa na kila mji, popote pale tangazo hili liliposomwa, Wayahudi walifurahi na kushangilia, wakafanya sherehe na mapumziko; na watu wengine wengi wakajifanya kuwa Wayahudi, maana waliwaogopa sana Wayahudi. Siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, ilipofika, siku ambayo tangazo la mfalme lingetekelezwa, na maadui wa Wayahudi walitarajia kuwashinda Wayahudi, iligeuzwa kuwa siku ya ushindi kwa Wayahudi dhidi ya adui zao. Katika kila mji wa kila mkoa wa mfalme Ahasuero, Wayahudi walijiandaa vizuri kumshambulia mtu yeyote ambaye angejaribu kuwadhuru. Ikawa viongozi wote wa mikoa, watawala, wakuu na maofisa wa mfalme pia waliwasaidia Wayahudi, maana wote walimwogopa Mordekai. Mordekai sasa alikuwa mtu mwenye madaraka makubwa katika ikulu, na habari zake zilienea katika mikoa yote kwamba uwezo wake ulikuwa unazidi kuongezeka. Basi, Wayahudi waliwashambulia maadui zao kwa upanga, wakawachinja, wakawaangamiza na kuwatenda kama walivyopenda. Huko mjini Susa, Wayahudi waliwaua watu 500. Pia waliwaua Parshandatha, Dalfoni, Aspatha, Poratha, Adalia, Aridatha, Parmashta, Arisai, Aridai na Waizatha, wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui ya Wayahudi. Hata hivyo, hawakuteka nyara. Siku hiyohiyo, mfalme alijulishwa idadi ya watu waliouawa katika mji mkuu wa Susa. Ndipo mfalme akamwambia malkia Esta: “Katika mji mkuu peke yake Wayahudi wamewaua watu 500, pamoja na wana kumi wa Hamani. Unafikiri wamefanyaje huko mikoani! Unataka nini sasa? Maana utatimiziwa. Niambie, unataka nini zaidi, nawe utapewa.” Esta akasema, “Ukiona ni vema, ewe mfalme, kesho waruhusu Wayahudi waliomo Susa wafanye kama agizo la leo lilivyokuwa. Tena, uamuru wana kumi wa Hamani watundikwe kwenye miti ya kuulia.” Mfalme akaamuru hayo yatekelezwe, na tangazo likatolewa mjini Susa. Wana kumi wa Hamani wakanyongwa hadharani. Siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, Wayahudi walikusanyika tena, wakawaua watu 300 zaidi mjini Susa. Lakini hawakuteka nyara mali za watu. Wayahudi waliokuwa katika mikoa nao pia walijiandaa kuyalinda maisha yao. Wakaokolewa kutoka kwa maadui wao; waliwaua watu wapatao 75,000, lakini hawakuchukua nyara. Siku hiyo ilikuwa ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari. Siku iliyofuata ya kumi na nne, walipumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na sherehe. Lakini Wayahudi wa mji mkuu wa Susa walikusanyika pia siku ya kumi na nne lakini hawakupumzika. Waliadhimisha siku ya kumi na tano kwa furaha na shangwe. Kutokana na sababu hii, Wayahudi wakaao vijijini na katika miji midogo huadhimisha siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kuwa sikukuu ya furaha, na kupelekeana zawadi hali wale waishio katika miji mikubwa huadhimisha siku ya kumi na tano ya mwezi wa Adari kama siku ya mapumziko, wakapelekeana pia zawadi. Mordekai aliandika matukio haya yote. Kisha aliwaandikia barua Wayahudi wote waliokuwa katika utawala wa Ahasuero. Aliwataka kila mwaka waadhimishe sikukuu, siku ya kumi na nne na siku ya kumi na tano ya mwezi wa Adari. Wayahudi waliwashinda maadui zao katika siku hizo, na katika mwezi huo huzuni yao iligeuzwa kuwa furaha, na misiba yao kuwa sikukuu. Waliagizwa wawe wakizikumbuka siku hizo kwa kufanya karamu na sherehe, kupelekeana zawadi za chakula na kuwapa maskini vitu. Basi, Wayahudi walikubaliana kufanya kama walivyoanza na kama Mordekai alivyowaandikia. Hamani mwana wa Hamedatha, wa Agagi na adui wa Wayahudi alikuwa amefanya hila dhidi ya Wayahudi kuwaangamiza, pia alikuwa amepiga Puri, yaani kura, ili kuamua siku ya kuwaponda na kuwaangamiza Wayahudi. Lakini Esta alipomwendea mfalme, naye mfalme alitoa amri kwa maandishi kwamba ile hila mbaya ambayo Hamani alikuwa amefanya dhidi ya Wayahudi, impate yeye mwenyewe; na ya kuwa yeye na wanawe wauawe kwa kutundikwa kwenye mti wa kuulia. Kwa hiyo, waliita siku hizo Purimu, kutokana na neno puri yaani kura. Kwa sababu ya barua ya Mordekai na mambo waliyoyaona wenyewe na yale yaliyowapata, Wayahudi waliifanya kuwa sheria rasmi kwao, kwa wazawa wao na kwa mtu yeyote ambaye angejiunga nao, kwamba katika wakati maalumu kila mwaka, bila kukosa, siku hizo mbili ziadhimishwe kulingana na maagizo ya Mordekai. Pia walikubaliana kwamba kila jamaa ya Kiyahudi, kizazi baada ya kizazi, katika kila mkoa na mji, sharti ikumbuke siku za Purimu na kuzisherehekea daima. Ndipo malkia Esta, binti Abihaili, akaandika barua kwa mamlaka yake yote, pamoja na Mordekai Myahudi kuthibitisha yale aliyoandika Mordekai hapo awali kuhusu Purimu. Barua hiyo waliandikiwa Wayahudi wote, na nakala zake kupelekewa mikoa yote 127 ya utawala wa Ahasuero. Barua hiyo iliwatakia Wayahudi amani na usalama, na kuwahimiza wao na wazawa wao waadhimishe sikukuu za Purimu kwa wakati wake maalumu, kama vile walivyokuwa wanazikumbuka sheria za kufunga wakati wa kuomboleza. Maagizo haya yalitolewa na Mordekai, Myahudi, pamoja na malkia Esta. Amri yake Esta ikathibitisha mambo hayo ya Purimu; ikaandikwa kitabuni. Mfalme Ahasuero alitoza kodi watu wa bara na pwani. Matendo yake yote makuu na ya ajabu, pamoja na simulizi kamili kuhusu jinsi alivyompandisha cheo Mordekai na kumtunukia heshima kuu, yote yameandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za wafalme wa Media na Persia. Mordekai, Myahudi, alikuwa wa kwanza chini ya mfalme Ahasuero katika madaraka. Alipendwa na kuheshimiwa na Wayahudi, maana aliwafanyia mema watu wake na kuwatakia amani wazawa wao wote. Palikuwa na mtu mmoja nchini Usi, aitwaye Yobu. Mtu huyo alikuwa mwema na mnyofu; mtu mcha Mungu na mwenye kuepukana na uovu. Yobu alikuwa na watoto saba wa kiume na watatu wa kike; alikuwa na kondoo 7,000, ngamia 3,000, jozi 500 za ng'ombe na punda majike 500; na watumishi wengi sana; yeye alikuwa mashuhuri kuliko watu wote huko mashariki. Mara kwa mara, wanawe Yobu walifanya karamu nyumbani kwa kila mmoja wao kwa zamu; waliwaalika dada zao kula na kunywa pamoja nao. Kila baada ya karamu, Yobu aliwaita wanawe ili awatakase. Aliamka asubuhi na mapema baada ya karamu, akatoa tambiko za kuteketezwa kwa ajili ya kila mmoja wao kwani aliwaza, “Huenda wanangu wametenda dhambi na kumtukana Mungu mioyoni mwao.” Basi, ikatokia siku moja malaika wa Mungu walikwenda kukutana mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye Shetani, akajitokeza pia pamoja nao. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Naye Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Nimetoka kutembeatembea na kuzungukazunguka duniani.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Bila shaka umemtambua mtumishi wangu Yobu. Duniani kote hamna mwingine aliye kama yeye. Yeye ni mtu mnyofu, mcha Mungu na mwenye kujiepusha na uovu.” Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Je, Yobu anamcha Mwenyezi-Mungu bure? Je, si dhahiri kwamba wewe unamlinda pande zote pamoja na jamaa yake na kila kitu alicho nacho? Wewe umembariki na mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini sasa, hebu nyosha tu mkono wako uiguse mali yake kama hutaona akikutukana waziwazi!” Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Haya, waweza kufanya chochote uwezacho juu ya mali yake; ila tu yeye mwenyewe usimguse.” Basi, Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Ikawa siku moja, watoto wa kiume na wa kike wa Yobu walikuwa wanakula na kunywa pamoja nyumbani kwa kaka yao mkubwa. Basi, mtumishi akafika kwa Yobu, akamwambia, “Tulikuwa tunalima kwa majembe ya kukokotwa na ng'ombe. Punda nao walikuwa wanakula hapo karibu. Basi Wasabea wakatuvamia na kuwachukua wanyama na kuwaua watumishi kwa upanga. Mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Kabla hajamaliza kusema, mwingine akawasili, akasema, “Umeme wa radi umewachoma na kuwateketeza kondoo na watumishi, mimi tu peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Huyo naye kabla hajamaliza kusema, mwingine akawasili, akasema, “Wakaldayo walijipanga makundi matatu wakashambulia ngamia, wakawachukua, na kuwaua watumishi wako kwa upanga! Mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Kabla hajamaliza kusema, akaja mwingine, akasema, “Watoto wako wa kiume na wa kike walikuwa wanakula na kunywa divai nyumbani kwa kaka yao mkubwa. Mara kimbunga kikavuma kutoka jangwani, kikaipiga nyumba hiyo kila upande nayo ikawaangukia, na vijana wote wamekufa, mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Kisha Yobu akasimama, akararua mavazi yake, akanyoa nywele zake, akajitupa chini na kumwabudu Mungu. Akasema, “Uchi nilikuja duniani, uchi nitaondoka duniani; Mwenyezi-Mungu amenipa, Mwenyezi-Mungu amechukua; litukuzwe jina lake Mwenyezi-Mungu.” Katika mambo haya yote Yobu hakutenda dhambi wala hakumfikiria Mungu kuwa ana kosa. Ikatokea tena siku nyingine, malaika wa Mungu walikwenda kukutana mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye Shetani akajitokeza pia pamoja nao. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Naye Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Nimetoka kutembeatembea na kuzungukazunguka duniani.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia mtumishi wangu Yobu? Duniani hakuna mwingine aliye kama yeye. Yeye ni mtu mnyofu, mcha Mungu na mwenye kujiepusha na uovu. Yeye yuko imara katika unyofu wake, ingawa wewe umenichochea nimwangamize bure.” Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Ngozi kwa ngozi! Mtu hutoa kila kitu alicho nacho ili aokoe uhai wake. Lakini sasa hebu nyosha mkono wako umguse mwili wake; nakuambia atakutukana waziwazi.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Haya! Waweza kumfanya utakavyo, walakini usimuue.” Hapo Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamtesa Yobu kwa madonda mabaya tangu wayo wa mguu wake mpaka utosini mwake. Yobu akatwaa kigae, akajikuna nacho na kuketi kwenye majivu. Mkewe akamwambia, “Bado tu ungali ukishikilia unyofu wako? Mtukane Mungu, ufe.” Yobu akamjibu mkewe, “Wewe unaongea kama wanawake wapumbavu. Tukipokea mema kutoka kwa Mungu, kwa nini tukatae kupokea pia mabaya kutoka kwake?” Katika mambo hayo yote, Yobu hakutamka neno lolote la kumkosea Mungu. Marafiki watatu wa Yobu: Elifazi kutoka Temani, Bildadi kutoka Shua na Sofari kutoka Naamathi, walisikia juu ya maafa yote yaliyompata Yobu. Basi, wakaamua kwa pamoja waende kumpa pole na kumfariji. Walipomwona kwa mbali hawakumtambua. Basi, wakaanza kupaza sauti na kulia; waliyararua mavazi yao, wakarusha mavumbi angani na juu ya vichwa vyao. Kisha wakaketi udongoni pamoja na Yobu kwa siku saba, mchana na usiku, bila kumwambia neno lolote kwani waliyaona mateso yake kuwa makubwa mno. Hatimaye Yobu aliamua kuongea, akailaani siku aliyozaliwa. Yobu akasema: “Ilaaniwe siku ile niliyozaliwa; usiku ule iliposemwa, ‘Mwana amechukuliwa mimba’ Siku hiyo na iwe giza! Mungu juu asijishughulishe nayo! Wala nuru yoyote isiiangaze! Mauzauza na giza nene yaikumbe, mawingu mazito yaifunike. Giza la mchana liitishe! Usiku huo giza nene liukumbe! Usihesabiwe katika siku za mwaka, wala usitiwe katika idadi ya siku za mwezi. Naam, usiku huo uwe tasa, sauti ya furaha isiingie humo. Walozi wa siku waulaani, watu stadi wa kuligutua dude Lewiyathani waulaani! Nyota zake za pambazuko zififie, utamani kupata mwanga, lakini usipate, wala usione nuru ya pambazuko. Maana usiku huo haukulifunga tumbo la mama, wala kuficha taabu nisizione. Mbona sikufa nilipozaliwa, nikatoka tumboni na kutoweka? Kwa nini mama yangu alinizaa? Kwa nini nikapata kunyonya? Maana ningekuwa nimezikwa, kimya; ningekuwa nimelazwa na kupumzika, pamoja na wafalme na watawala wa dunia, waliojijengea upya magofu yao; ningekuwa pamoja na wakuu waliokuwa na dhahabu, waliojaza nyumba zao fedha tele. Au, mbona sikuwa kama mimba iliyoharibika, naam, kama mtoto aliyezaliwa mfu? Huko kwa wafu waovu hawamsumbui mtu, huko wachovu hupumzika. Huko wafungwa hustarehe pamoja, hawaisikii kamwe sauti ya mnyapara. Wakubwa na wadogo wako huko, nao watumwa wamepata uhuru mbali na bwana zao. Ya nini kumjalia nuru yule aliye taabuni; na uhai yule aliye na huzuni moyoni? Mtu atamaniye kifo lakini hafi; hutafuta kifo kuliko hazina iliyofichika. Mtu kama huyo atashangilia mno na kufurahi, atafurahi atakapokufa na kuzikwa! Ya nini kumjalia uhai mtu ambaye njia zake zimefungwa, mtu ambaye Mungu amemwekea kizuizi? Kwa maana kusononeka ndio mkate wangu, kupiga kite kwangu kunatiririka mithili ya maji. Kile ninachokiogopa kimenipata, ninachokihofia ndicho kilichonikumba. Sina amani wala utulivu; sipumziki, taabu imenijia.” Kisha Elifazi yule Mtemani akamjibu Yobu: “Je, mtu akijaribu kukuambia neno utakasirika? Lakini nani awezaye kujizuia kusema? Sikiliza! Wewe umewafundisha wengi, na kuiimarisha mikono ya wanyonge. Maneno yako yamewainua waliokufa moyo, umewaimarisha waliokosa nguvu. Lakini sasa yamekupata, nawe ukakosa subira, yamekugusa, nawe ukafadhaika. Je, kumcha Mungu si ndilo tegemeo lako? Na unyofu wako si ndilo tumaini lako? Fikiri sasa: Nani asiye na hatia ambaye amepata kuangamia? Au, je, waadilifu wamepata kutupwa? Nijuavyo mimi, wapandao uovu na ubaya huvuna hayohayo, Mungu huwaangamiza hao kwa pumzi yake, hao huteketezwa kwa pigo la hasira yake. Waovu hunguruma kama simba mkali, lakini meno yao huvunjwa. Simba mwenye nguvu hufa kwa kukosa mawindo, na watoto wa simba jike hutawanywa! “Siku moja, niliambiwa neno kwa siri, sikio langu lilisikia mnongono wake. Nikiwa katika mawazo ya njozi za usiku, wakati usingizi mzito huwashika watu, nilishikwa na hofu na kutetemeka, mifupa yangu yote ikagonganagongana. Upepo ukapita mbele ya uso wangu, nywele za mwilini mwangu zikajisimamisha. Kitu kilisimama tuli mbele yangu, nilipokitazama sikukitambua kabisa. Kulikuwa na umbo fulani mbele yangu; kulikuwa kimya, kisha nikasikia sauti. Binadamu afaye aweza kuwa mwadilifu mbele ya Mungu? Mtu aweza kuwa safi mbele ya Muumba wake? Hata watumishi wake, Mungu hana imani nao; na malaika wake huwaona wana kosa; sembuse binadamu viumbe vya udongo, watu ambao chanzo chao ni mavumbi, ambao waweza kupondwapondwa kama nondo! Binadamu kwa masaa machache tu waweza kuangamia; huangamia milele bila kuacha hata alama yao! Iwapo uzi unaoshikilia uhai wao ukikatwa wao hufa tena bila kuwa na hekima. “Ita sasa, uone kama kuna wa kukuitikia. Ni yupi kati ya watakatifu utakayemwita? Ama kweli hangaiko humuua mpumbavu, na wivu humwangamiza mjinga. Nimepata kuona mpumbavu akifana, lakini ghafla nikayalaani makao yake. Watoto wake hawana usalama; hudhulumiwa mahakamani, na hakuna mtu wa kuwatetea. Mazao yake huliwa na wenye njaa, hata nafaka iliyoota kati ya miiba; wenye tamaa huuonea shauku utajiri wake. Kwa kawaida mateso hayatoki mavumbini wala matatizo hayachipui udongoni. Bali binadamu huzaliwa apate taabu, kama cheche za moto zirukavyo juu. “Kama ningekuwa wewe ningemgeukia Mungu, ningemwekea yeye Mungu kisa changu, yeye atendaye makuu yasiyochunguzika, atendaye maajabu yasiyohesabika. Huinyeshea nchi mvua, hupeleka maji mashambani. Huwainua juu walio wanyonge, wenye kuomboleza huwapa usalama. Huvunja mipango ya wenye hila, matendo yao yasipate mafanikio. Huwanasa wenye hekima kwa werevu wao, mipango ya wajanja huikomesha mara moja. Hao huona giza wakati wa mchana, adhuhuri hupapasapapasa kama vile usiku. Lakini Mungu huwaokoa yatima wasiuawe, huwanyakua fukara mikononi mwa wenye nguvu. Hivyo maskini wanalo tumaini, nao udhalimu hukomeshwa. “Heri mtu yule ambaye Mungu anamrudi! Hivyo usidharau Mungu Mwenye Nguvu anapokuadhibu. Kwani yeye huumiza na pia huuguza; hujeruhi, na kwa mkono wake huponya. Atakuokoa katika maafa zaidi ya mara moja; katika balaa la mwisho, uovu hautakugusa. Wakati wa njaa atakuokoa na kifo, katika mapigano makali atakuokoa. Utakingwa salama na mashambulio ya ulimi, wala hutaogopa maangamizi yajapo. Maangamizi na njaa vijapo, utacheka, wala hutawaogopa wanyama wakali wa nchi. Nawe utaafikiana na mawe ya shambani, na wanyama wakali watakuwa na amani nawe. Utaona nyumbani mwako mna usalama; utakagua mifugo yako utaiona yote ipo. Utaona pia wazawa wako watakuwa wengi, wengi kama nyasi mashambani. Utafariki ukiwa mkongwe mtimilifu, kama mganda wa ngano ya kupurwa iliyoiva vizuri. Basi huu ndio utafiti wetu; tena ni ukweli; uusikie na kuuelewa kwa faida yako.” Yobu akamjibu Elifazi: “Laiti mahangaiko yangu yangepimwa uzani wake, mateso yangu yote yakawekwa katika mizani! Yangekuwa mazito kuliko mchanga wa pwani. Ndio maana maneno yangu ni ya kuropoka! Naam, mishale ya Mungu Mwenye Nguvu imenichoma; nafsi yangu imekunywa sumu yake. Vitisho vya Mungu vimenikabili. Je, pundamwitu hulia akiwa na majani, au ng'ombe akiwa na malisho? Je, kitu kisicho na ladha chaweza kuliwa bila chumvi? Je ute wa yai una utamu wowote? Sina hamu ya kuvigusa vyakula hivyo, hivyo ni vyakula vyangu vichukizavyo. ” “Laiti ningejaliwa ombi langu, Mungu akanipatia kile ninachotamani: Kwamba angekuwa radhi kunipondaponda, angenyosha mkono wake anikatilie mbali! Hiyo ingekuwa faraja yangu, ningefurahi katika maumivu yasiyo na huruma. Lakini sina nguvu ya kuweza kuendelea; sijui mwisho wangu utakuwaje, nipate kuvumilia. Je, nguvu zangu ni kama za mawe? Au mwili wangu kama shaba? Kweli kwangu hamna cha kunisaidia; msaada wowote umeondolewa kwangu. “Anayekataa kumhurumia rafiki yake, anakataa kumcha Mungu mwenye nguvu. Rafiki zangu wamenidanganya kama kijito, wamenihadaa kama mitaro isiyo na maji. Ambayo imejaa barafu, na theluji imejificha ndani yake. Lakini wakati wa joto hutoweka, wakati wa hari hubaki mito mikavu. Misafara hupotea njia wakitafuta maji, hupanda nyikani na kufia huko. Misafara ya Tema hutafuta tafuta, wasafiri wa Sheba hutumaini. Huchukizwa kwa kutumaini bure, hufika kwenye vijito hivyo na kuudhika. Nyinyi mmekuwa kama vijito hivyo, mwaona balaa yangu na kuogopa. Je, nimesema mnipe zawadi? Au mnitolee rushwa kwa mali zenu? Au mniokoe makuchani mwa adui? Au mnikomboe mkononi mwa wadhalimu? “Nifundisheni, nami nitanyamaza. Nielewesheni jinsi nilivyokosea. Maneno ya kweli yana nguvu kubwa! Lakini makaripio yenu yananikosoa nini? Je, mnadhani kwamba mwaweza kuyakosoa maneno? Maneno ya mtu aliyekata tamaa ni upepo tu. Nyinyi mnathubutu hata kuwapigia yatima kura; mnawapigia bei hata marafiki zenu! Lakini sasa niangalieni tafadhali. Mimi sitasema uongo mbele yenu. Acheni tafadhali, kusiwe na uovu; acheni sasa, kwani mimi ni mnyofu. Je, mnadhani kwamba nimesema uovu? Je, mnafikiri mimi siyatambui machungu? “Binadamu anayo magumu duniani, na siku zake ni kama siku za kibarua! Yeye ni kama mtumwa atamaniye kivuli, kama mwajiriwa angojaye kwa hamu mshahara wake. Basi nimepangiwa miezi na miezi ya ubatili, yangu ni majonzi usiku hata usiku. Nilalapo nasema, ‘Nitaamka lini?’ Kwani saa za usiku huwa ndefu sana; nagaagaa kitandani mpaka kuche! Mwili wangu umejaa mabuu na uchafu; ngozi yangu imekauka na kutokwa na usaha wa jipu. Siku zangu zapita kasi kuliko gurudumu la mshonaji, nazo zafikia mwisho wake bila matumaini. “Kumbuka, maisha yangu ni pumzi tu; jicho langu halitaona jema lolote tena. Anayeniona sasa, hataniona tena, punde tu ukinitazama nitakuwa nimetoweka. Kama wingu lififiavyo na kutoweka ndivyo nao watu washukavyo kuzimu bila kurudi. Anayeondoka harudi tena kwa jamaa yake, na pale alipokuwa anaishi husahaulika mara. “Kwa hiyo sitakizuia kinywa changu kuongea; nitasema kwa msongo wa roho yangu, nitalalamika kwa uchungu wa nafsi yangu. Je, mimi ni bahari au dude la baharini hata uniwekee mlinzi? Nikisema, ‘Kitanda kitanipumzisha, malazi yangu yatanipunguzia malalamiko yangu,’ wewe waja kunitia hofu kwa ndoto, wanitisha kwa kuniletea maono; hata naona afadhali kujinyonga, naona heri kufa kuliko kupata mateso haya. Nayachukia maisha yangu; sitaishi milele. Niacheni, maana siku zangu ni pumzi tu! Binadamu ni nini hata umjali? Kwa nini hata unajishughulisha naye? Wewe waja kumchunguza kila asubuhi, kila wakati wafika kumjaribu! Utaendelea kuniangalia hata lini, bila kuniacha hata nimeze mate? Kama nikitenda dhambi, yakudhuru nini ewe mkaguzi wa binadamu? Mbona umeniweka kuwa shabaha ya mapigo yako? Je, mimi nimekuwa mzigo kwako? Mbona hunisamehi kosa langu na kuniondolea uovu wangu? Hivi punde nitalazwa chini kaburini, utanitafuta, lakini sitakuwapo tena!” Ndipo Bildadi, Mshuhi, akamjibu Yobu: “Utasema mambo haya mpaka lini? Mpaka lini maneno yako yatakuwa matupu kama upepo? Kwani, wadhani Mungu hupotosha haki? Au, je, Mungu Mwenye Nguvu hupotosha ukweli? Kama watoto wako wamemkosea Mungu, yeye amewalipiza matokeo ya uhalifu wao. Kama utamtafuta Mungu ukamsihi huyo Mungu mwenye nguvu, kama wewe u safi moyoni na mnyofu, kweli Mungu atakuja kukusaidia, na kukujalia makao unayostahili. Na ingawa ulianza kuishi kwa unyonge maisha yako ya baadaye yatakuwa ya fahari zaidi. Jifunze tafadhali kwa wale waliotutangulia, zingatia mambo waliyogundua hao wazee. Sisi ni watu wa juzijuzi tu, hatujui kitu; siku zetu duniani ni kivuli kipitacho. Lakini wao watakufunza na kukuambia, mambo waliyopata kuyatoa katika maarifa yao: Mafunjo huota tu penye majimaji, matete hustawi mahali palipo na maji. Hata kama yamechanua na bila kukatwa, yakikosa maji hunyauka kabla ya mimea mingine. Ndivyo walivyo wote wanaomsahau Mungu. Tumaini la wasiomwamini Mungu litapotea. Tegemeo lao huvunjikavunjika, tumaini lao ni utando wa buibui. Wanaegemea nyumba yao lakini haitasimama, huishikilia lakini haidumu. Jua litokapo yeye hustawi; hueneza matawi yake bustanini mwake. Mizizi yake hujisokotasokota kwenye mawe naye aenda kuchunguza ndani ya mwamba. Lakini akiangamizwa kutoka makao yake, hayo yatamkana yakisema: ‘Sijapata kukuona.’ Tazama, huo ndio mwisho wa furaha ya mtu huyo, na mahali pao patachipua wengine. “Tazama! Mungu hatamkataa mtu asiye na hatia, wala kuwasaidia waovu. Ila atakijaza kinywa chako kicheko, na midomo yako sauti ya furaha. Wale wakuchukiao wataingiwa na aibu, makao ya waovu yatatoweka kabisa.” Kisha Yobu akajibu: “Kweli najua hivyo ndivyo ilivyo. Lakini mtu awezaje kuwa mwema mbele ya Mungu? Kama mtu angethubutu kushindana naye, hataweza kufika mbali; hata kujibu swali moja kati ya elfu. Yeye ni mwenye hekima mno na nguvu nyingi, nani aliyepingana naye, akashinda? Yeye huiondoa milima bila yenyewe kutambua, huibomolea mbali kwa hasira yake. Yeye huitikisa dunia kutoka mahali pake, na nguzo zake zikatetemeka. Huliamuru jua lisichomoze huziziba nyota zisiangaze. Yeye peke yake alizitandaza mbingu, na kuyakanyaga mawimbi ya bahari. Ndiye aliyezifanya nyota angani: Dubu, Orioni, Kilimia, na nyota za kusini. Ndiye atendaye makuu yasiyoeleweka, mambo ya ajabu yasiyo na idadi. Loo! Hupita karibu nami nisimwone, kisha huenda zake bila ya mimi kumtambua. Tazama! Yeye huchukua anachotaka; nani awezaye kumzuia? Nani awezaye kumwuliza: ‘Unafanya nini?’ “Mungu hatazuia hasira yake; chini yake wainama kwa hofu Rahabu na wasaidizi wake. Nitawezaje basi kumjibu Mungu? Nitachagua wapi maneno ya kumwambia? Ingawa sina hatia, siwezi kumjibu. Lazima kumwomba anihurumie huyo mshtaki wangu. Hata kama ningemwita naye akajibu, nisingeweza kuamini kuwa ananisikiliza. Yeye huniponda kwa dhoruba; huongeza majeraha yangu bila sababu. Haniachi hata nipumue; maisha yangu huyajaza uchungu. Kama ni kushindana, yeye ana nguvu mno! Na kama ni kutafuta juu ya haki, nani atakayemleta mahakamani? Ingawa sina hatia, maneno yangu yenyewe yangenihukumu; ingawa sina lawama, angenithibitisha kuwa mpotovu. Sina lawama, lakini sijithamini. Nayachukia maisha yangu. Yote ni mamoja, kwa hiyo nasema; Mungu huwaangamiza wema na waovu. Maafa yaletapo kifo cha ghafla, huchekelea balaa la wasio na hatia. Nchi ikitiwa watu waovu katika utawala wa mwovu, Mungu huyafumba macho ya mahakimu wake! Kama si yeye afanyaye hivyo, ni nani basi? “Siku zangu zaenda mbio kuliko mpiga mbio; zinakimbia bila kuona faida. Zapita kasi kama mashua ya matete; kama tai anayerukia mawindo yake. Nasema: ‘Nitasahau lalamiko langu, niondoe uso wangu wa huzuni na kuwa na furaha!’ Lakini nayaogopa maumivu yangu yote, kwani najua Mungu hataniona kuwa sina hatia. Ikiwa nitahukumiwa kuwa na hatia, ya nini basi nijisumbue bure? Hata kama nikitawadha kwa theluji, na kujitakasa mikono kwa sabuni, hata hivyo, atanitumbukiza shimoni kwenye uchafu, na mavazi yangu yataniona kuwa kinyaa. Mungu si mtu kama mimi niweze kumjibu, hata tuweze kwenda mahakamani pamoja. Hakuna msuluhishi kati yetu, ambaye angeamua kati yetu sisi wawili. Mungu na aniondolee hiyo fimbo ya kunipiga, na kitisho chake kisinitie hofu! Hapo ningeweza kusema bila kumwogopa; kwani sivyo nilivyo nafsini mwangu. “Nayachukia maisha yangu! Malalamiko yangu nitayasema bila kizuizi. Nitasema kwa uchungu wa moyo wangu. Nitamwambia Mungu: Usinihukumu. Nijulishe kisa cha kupingana nami. Je, ni sawa kwako kunionea, kuidharau kazi ya mikono yako na kuipendelea mipango ya waovu? Je, una macho kama ya binadamu? Je, waona kama binadamu aonavyo? Je, siku zako ni kama za binadamu? Au miaka yako kama ya binadamu, hata uuchunguze uovu wangu, na kuitafuta dhambi yangu? Wewe wajua kwamba mimi sina hatia, na hakuna wa kuniokoa mikononi mwako. Mikono yako iliniunda na kuniumba, lakini sasa wageuka kuniangamiza. Kumbuka kwamba uliniumba kwa udongo. Je, utanirudisha tena mavumbini? Je, si wewe uliyenimimina kama maziwa, na kunigandisha kama jibini? Uliuumba mwili wangu kwa mifupa na mishipa, ukaifunika mifupa yangu kwa nyama na ngozi. Umenijalia uhai na fadhili, uangalifu wako umeisalimisha nafsi yangu. Hata hivyo mambo haya uliyaficha moyoni. Lakini najua kuwa hiyo ilikuwa nia yako. Ulikuwa unangojea uone kama nitatenda dhambi, ili ukatae kunisamehe uovu wangu. Kama mimi ni mwovu, ole wangu! Kama mimi ni mwadilifu, siwezi kujisifu; kwani nimejaa fedheha, nikiyatazama mateso yangu. Nikiinua kichwa tu waniwinda kama simba na kuniponda tena kwa maajabu yako. Kila mara unao ushahidi dhidi yangu; waiongeza hasira yako dhidi yangu, waniletea maadui wapya wanishambulie. “Ee Mungu, kwa nini ulinitoa tumboni mwa mama? Afadhali ningekufa kabla ya watu kuniona. Ningepelekwa moja kwa moja kaburini, nikawa kama mtu asiyepata kuwako. Je, siku za maisha yangu si chache? Niachie nipate faraja kidogo, kabla ya kwenda huko ambako sitarudi, huko kwenye nchi ya huzuni na giza nene; nchi ya huzuni na fujo, ambako mwanga wake ni kama giza.” Kisha Sofari, Mnaamathi, akamjibu Yobu: “Je, wingi huu wa maneno uachwe tu bila kujibiwa? Je, mtu wa maneno mengi aonesha kuwa hana hatia? Je, kuropoka kwako kutanyamazisha watu? Na kama ukidhihaki, je, hamna atakayekuaibisha? Wewe wadai: ‘Ninachosema ni kweli, naam, sina lawama mbele ya Mungu.’ Laiti Mungu angefungua kinywa chake akatoa sauti yake kukujibu! Angekueleza siri za hekima, maana yeye ni mwingi wa maarifa. Jua kwamba Mungu hakuhesabu makosa yako yote. “Je, unaweza kugundua siri zake Mungu na kujua ukomo wake yeye Mungu mwenye nguvu? Ukuu wake wapita mbingu, wewe waweza nini? Kimo chake chapita Kuzimu, wewe waweza kujua nini? Ukuu huo wapita marefu ya dunia, wapita mapana ya bahari. Kama Mungu akipita, akamfunga mtu na kumhukumu, nani awezaye kumzuia? Mungu anajua watu wasiofaa; akiona maovu yeye huchukua hatua. “Mpumbavu hawezi kuwa na maarifa, pundamwitu ni pundamwitu tu. “Yobu, ukiufanya moyo wako mnyofu, utainua mikono yako kumwomba Mungu! Kama una uovu, utupilie mbali. Usikubali ubaya uwemo nyumbani mwako. Hapo utajitokeza mbele ya watu bila lawama, utakuwa thabiti bila kuwa na hofu. Utazisahau taabu zako zote; utazikumbuka tu kama mafuriko yaliyopita. Maisha yako yatangaa kuliko jua la adhuhuri, giza lake litabadilika kuwa mngao wa pambazuko. Utakuwa na ujasiri maana lipo tumaini; utalindwa na kupumzika salama. Utalala bila kuogopeshwa na mtu; watu wengi watakuomba msaada. Lakini waovu macho yao yatafifia, njia zote za kutorokea zitawapotea; tumaini lao la mwisho ni kukata roho!” Ndipo Yobu akajibu: “Sawa! Nyinyi ni watu wa hekima. Hekima itakufa wakati ule mtakapokufa. Mimi nami ni mwelewa kama nyinyi. Mimi si mtu duni kuliko nyinyi. Yote mliyosema kila mtu anajua. Nimekuwa kichekesho kwa rafiki zangu: Mimi niliyemwomba Mungu na akanijibu; mimi niliye mwadilifu na bila lawama, nimekuwa kichekesho kwa watu. Mtu anayestarehe hudharau msiba; kwake, msiba huwajia wale wanaoteleza. Makao ya wanyanganyi yana amani; wenye kumchokoza Mungu wako salama, nguvu yao ni mungu wao. Lakini waulize wanyama nao watakufunza; waulize ndege nao watakuambia. Au iulize mimea nayo itakufundisha; sema na samaki nao watakuarifu. Nani kati ya viumbe hivyo, asiyejua kwamba Mwenyezi-Mungu ametenda hayo? Uhai wa kila kiumbe hai umo mikononi mwake; kadhalika na pumzi ya uhai wa binadamu. Je, sikio haliyapimi maneno kama ulimi uonjavyo chakula? Hekima iko kwa watu wazee, maarifa kwao walioishi muda mrefu. Lakini hekima na uwezo ni vyake Mungu, yeye ana maarifa na ujuzi. Akibomoa, hakuna awezaye kujenga upya; akimfunga mtu, hakuna awezaye kumfungua. Akizuia mvua, twapata ukame; akiifungulia, nchi hupata mafuriko. Yeye ana nguvu na hekima; wanaodanganywa na wanaodanganya ni wake. Huwaacha washauri waende zao uchi, huwafanya waamuzi kuwa wapumbavu. Huwavua wafalme vilemba vyao; na kuwafunga viunoni kamba za wafungwa; Huwaacha makuhani waende uchi; na kuwaangusha wenye nguvu. Huwanyanganya washauri kipawa chao cha kuongea, huwapokonya wazee hekima yao. Huwamwagia wakuu aibu, huwaondolea wenye uwezo nguvu zao. Huvifunua vilindi vya giza, na kuleta mwangani yaliyokuwa gizani. Huyakuza mataifa kisha huyaangamiza, huyafanya yapanuke kisha huyatawanya. Huwaondolea viongozi wa watu ujuzi wao, huwafanya watangetange nyikani kusiko na njia, wakapapasapapasa gizani kusiko na mwanga; na kuwafanya wapepesuke kama walevi. “Tazama, hayo yote nimeyaona kwa macho yangu; nimeyasikia kwa masikio yangu mwenyewe na kuelewa. Yote mnayoyajua, mimi pia nayajua. Mimi si mtu duni kuliko nyinyi. Lakini ningependa kusema na Mungu mwenye nguvu, natamani kujitetea mbele zake Mungu. Lakini nyinyi mnaupakaa uongo chokaa; nyinyi nyote ni waganga wasiofaa kitu. Laiti mngekaa kimya kabisa, ikafikiriwa kwamba mna hekima! Sikilizeni basi hoja yangu, nisikilizeni ninapojitetea. Je, mnadhani mwamtumikia Mungu kwa kusema uongo? Mnafikiri kusema kwa hila kunamfaa yeye? Je, mnajaribu kumpendelea Mungu? Je, mtamtetea Mungu mahakamani? Je, akiwakagua nyinyi mtapona? Au mnadhani mnaweza kumdanganya Mungu kama watu? Hakika yeye atawakemea kama mkionesha upendeleo kwa siri. Je, fahari yake haiwatishi? Je, hampatwi na hofu juu yake? Misemo yenu ni methali za majivu, hoja zenu ni ngome za udongo. “Nyamazeni, nami niongee. Yanipate yatakayonipata. Niko tayari hata kuhatarisha maisha yangu; Mungu aniue akitaka, sina la kupoteza, hata hivyo nitautetea mwenendo wangu mbele yake. Kama nikifaulu hapo nitakuwa nimeshinda, maana mtu mwovu hawezi kwenda mbele yake. Sikilizeni kwa makini maneno yangu, maelezo yangu na yatue masikioni mwenu. Kesi yangu nimeiandaa vilivyo, nina hakika mimi sina hatia. “Nani atakayeipinga hoja yangu? Niko tayari kunyamaza na kufa. Mungu wangu, nijalie tu haya mawili, nami sitajificha mbali na wewe: Kwanza uniondolee mkono wako unaonipiga, na usiniangamize kwa kitisho chako. “Uanze kutoa hoja yako nami nikujibu. Au mimi nianze, nawe unijibu. Makosa na dhambi zangu ni ngapi? Nijulishe hatia na dhambi yangu. “Mbona unaugeuza uso wako mbali nami? Kwa nini unanitendea kama adui yako? Je, utalitisha jani linalopeperushwa, au kuyakimbiza makapi? Wewe umetoa mashtaka makali dhidi yangu, na kunibebesha dhambi za ujana wangu. Wanifunga minyororo miguuni, wazichungulia hatua zangu zote, na nyayo zangu umeziwekea kikomo. Nami naishia kama mti uliooza, mithili ya vazi lililoliwa na nondo. “Mtu ni mtoto tu wa mwanamke; huishi siku chache tena zilizojaa taabu. Huchanua kama ua, kisha hunyauka. Hukimbia kama kivuli na kutoweka. Ee Mungu, kwa nini unajali hata kumwangalia na kuanza kuhojiana naye? Nani awezaye kutoa kitu kisafi kutoka kitu kichafu? Hakuna anayeweza. Siku za kuishi binadamu zimepimwa; ee, Mungu umeipanga idadi ya miezi yake; hawezi kupita kikomo ulichomwekea. Angalia pembeni basi, umwache; ili apate kufurahia siku zake kama kibarua. Maana mti ukikatwa lipo tumaini la kuota, waweza kuchipua tena. Japo mizizi yake itazeeka udongoni, na shina lake kufia ardhini, lakini kwa harufu tu ya maji utachipua; utatoa matawi kama chipukizi. Lakini mtu hufa na huo ndio mwisho wake. Akisha toa roho anabakiwa na nini tena? “Kama vile maji yakaukavyo ziwani, na mto unavyokoma kutiririka, ndivyo anavyokufa mtu, wala haamki tena; hataamka tena wala kugutuka, hata hapo mbingu zitakapotoweka. “Laiti ungenificha kuzimu; ungenificha hadi ghadhabu yako ipoe; nao muda ulionipimia ukiisha ungenikumbuka. Je, mtu akifa anaweza kuishi tena? Siku zangu zote za kazi ningekungoja hadi wakati wa kufunguliwa ufike. Hapo ungeniita, nami ningeitika, wakati ungetaka kuniona mimi kiumbe chako. Ndipo ungeweza kuzihesabu hatua zangu, ungeacha kuzichunguza dhambi zangu. Makosa yangu yangefungiwa katika mfuko, nawe ungeufunika uovu wangu. “Lakini milima huanguka majabali hungoka mahali pake. Mtiririko wa maji hula miamba, mvua kubwa hufanya mmomonyoko wa ardhi. Ndivyo nawe unavyoharibu tumaini la binadamu. Wewe wamwangusha binadamu, naye akatoweka milele; waubadilisha uso wake na kumtupilia mbali. Watoto wake wakiheshimika, yeye hana habari. Wakiporomoshwa, yeye haoni kabisa. Huhisi tu maumivu ya mwili wake, na kuomboleza tu hali yake mbaya.” Kisha Elifazi, Mtemani, akajibu: “Je, mtu wa hekima hujibu kwa maneno ya upuuzi? Je, mtu huyo amejaa maneno matupu? Je, mwenye hekima hujitetea kwa maneno yasiyofaa, au kwa maneno yasiyo na maana? Lakini wewe unapuuza uchaji wa Mungu; na kuzuia kutafakari mbele ya Mungu. Uovu wako ndio unaokifundisha kinywa chako, nawe wachagua kusema kama wadanganyifu. Maneno yako mwenyewe yanakuhukumu, sio mimi; matamshi yako yashuhudia dhidi yako. Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa? Je, wewe ulizaliwa kabla ya kuweko vilima? Je, ulipata kuweko katika halmashauri ya Mungu? au, wewe ndiwe peke yako mwenye hekima? Unajua kitu gani tusichokijua sisi? Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi? Miongoni mwetu wapo wazee wenye hekima, wenye miaka mingi kuliko baba yako. Je, faraja anazokupa Mungu ni ndogo mno? Au je, neno lake la upole kwako si kitu? Mbona moyo unakusukuma kukasirika na kutoa macho makali, hata kumwasi Mungu na kusema maneno mabaya kama hayo? Mtu ni nini hata aweze kuwa mwadilifu? au yule aliyezaliwa na mwanamke hata aweze kuwa mwema? Ikiwa Mungu hawaamini hata watakatifu wake, nazo mbingu si safi mbele yake, sembuse binadamu aliye kinyaa na mpotovu binadamu atendaye uovu kama kunywa maji! “Sasa nisikilize, nami nitakuonesha, nitakuambia yale niliyoyaona, mafundisho ya wenye hekima, mambo ambayo wazee wao hawakuyaficha, ambao Mungu aliwapa hiyo nchi peke yao, wala hakuna mgeni aliyepita miongoni mwao. Mwovu atateseka kwa maumivu siku zote, miaka yote waliyopangiwa wakatili. Sauti za vitisho zitampigia kelele masikioni, anapodhani amestawi mwangamizi atamvamia. Mwovu hana tumaini la kutoka gizani; mwisho wake ni kufa kwa upanga. Hutangatanga kutafuta chakula, akisema, ‘Kiko wapi?’ Ajua kwamba siku ya giza inamkaribia. Taabu na uchungu, vyamtisha; vyamkabili kama jeshi la mfalme anayeshambulia. Kwa sababu amenyosha mkono wake dhidi ya Mungu; akadiriki kumpinga huyo Mungu mwenye nguvu; alikimbia kwa kiburi kumshambulia, huku ana ngao yenye mafundo makubwa. Uso wake ameunenepesha kwa mafuta, na kiuno chake kimejaa mafuta. Ameishi katika miji iliyoachwa tupu, katika nyumba zisizokaliwa na mtu; nyumba zilizotakiwa ziwe lundo la uharibifu. Mtu huyo kamwe hatakuwa tajiri; wala utajiri wake hautadumu duniani. Hatalikwepa giza la kifo. Ndimi za moto zitakausha chipukizi zake, maua yake yatapeperushwa na upepo. Heri aache kutumainia upuuzi na kujidanganya, maana upuuzi ndio utakaokuwa tuzo lake. Atalipwa kikamilifu kabla ya kufa kwake, na wazawa wake hawatadumu. Atakuwa kama mzabibu unaopukutisha zabibu mbichi, kama mzeituni unaoangusha maua yake. Wote wasiomcha Mungu hawatapata watoto, moto utateketeza mahema ya wala rushwa. Wanatunga udanganyifu na kuzaa uovu. Mioyo yao hupanga udanganyifu.” Hapo Yobu akajibu: “Mambo kama hayo nimeyasikia mengi; nyinyi ni wafariji duni kabisa! Mwisho wa maneno haya matupu ni lini? Au ni kitu gani kinachowachochea kujibu? Kama nyinyi mngekuwa mimi, na mimi nyinyi, ningeweza kusema kama nyinyi ningeweza kubuni maneno dhidi yenu, na kutikisa kichwa changu. Ningeweza kuwatia moyo kwa maneno yangu, na maneno yangu ya faraja yangewatuliza. “Lakini nikisema maumivu yangu hayatulii, na nikikaa kimya hayaondoki. Kweli Mungu amenichakaza ameharibu kila kitu karibu nami. Amenifanya ninyauke, na huo ni ushindi dhidi yangu. Kukonda kwangu kumenikabili na kushuhudia dhidi yangu. Amenirarua kwa hasira na kunichukia; amenisagia meno; na adui yangu ananikodolea macho. Watu wananidhihaki na kunicheka; makundi kwa makundi hunizunguka, na kunipiga makofi mashavuni. Mungu amenitia mikononi mwa wajeuri, na kunitupa mikononi mwa waovu. Nilikuwa nimestarehe, lakini akanivunjavunja, alinikaba shingo na kunipasua vipandevipande; alinifanya shabaha ya mishale yake, akanipiga mishale kutoka kila upande. Amenipasua figo bila huruma, na nyongo yangu akaimwaga chini. Hunivunja na kunipiga tena na tena; hunishambulia kama askari. “Nimejishonea mavazi ya gunia, fahari yangu nimeibwaga mavumbini. Uso wangu ni mwekundu kwa kulia, kope zangu zimekuwa nyeusi ti; ingawa sijafanya dhuluma kwa mkono wangu, na sala zangu kwa Mungu ni safi. “Ewe dunia, usiifunike damu yangu iliyomwagika; kilio changu kienee kila mahali. Nina hakika ninaye shahidi wangu mbinguni, mwenye kunitetea yuko huko juu. Rafiki zangu wanidharau; nabubujika machozi kumwomba Mungu. Laiti mtu angenitetea mbele ya Mungu, kama ifanyikavyo duniani kati za watu wawili. Naam, miaka yangu ni michache, nami nitakwenda huko ambako sitarudi. “Nimevunjika moyo, siku zangu zimekwisha, kaburi langu liko tayari. Kweli wanaonidhihaki wamenizunguka, dhihaka zao naziona dhahiri. “Ee Mungu, uwe mdhamini wangu mbele yako, maana hakuna mwingine wa kunidhamini. Maadamu umezifumba akili za rafiki zangu; usiwaache basi wanishinde. Mtu anayewasaliti rafiki zake kwa faida watoto wake watakufa macho. “Nimefanywa kuwa kichekesho kwa watu nimekuwa mtu wa kutemewa mate. Macho yangu yamefifia kwa uchungu; viungo vyangu vyote vimekuwa kama kivuli. Wanyofu wanaduwaa waonapo balaa langu, nao wasio na hatia hujichochea dhidi ya mtu wanayedhani hamchi Mungu. Hata hivyo, mnyofu hushikilia msimamo wake, mtu atendaye mema huzidi kuwa na nguvu zaidi. Lakini nyinyi njoni, njoni nyote tena, kwenu sitampata mwenye hekima hata mmoja. “Siku zangu zimekwisha, mipango yangu imevunjwa; matazamio ya moyo wangu yametoweka. Kwa hao rafiki zangu usiku ni mchana; je, ndio kusema mna mwanga gizani humu? Kwa vile Kuzimu ndio nyumba yangu, na makao yangu yamo humo gizani; kama naliita kaburi ‘baba yangu’ na buu, ‘mama yangu’ au ‘dada yangu’, je, nimebakiwa na tumaini gani? Ni nani awezaye kuona tumaini hilo? Tazamio langu litashuka nami kuzimu! Tutateremka sote wawili hadi huko mavumbini!” Kisha Bildadi, Mshuhi, akajibu: “Utawinda maneno ya kusema hadi lini? Tafakari vizuri nasi tutasema. Kwa nini unatufanya kama ng'ombe? Mbona unatuona sisi kuwa wapumbavu? Wewe unajirarua mwenyewe kwa hasira zako. Kwani, dunia itaachwa tupu kwa ajili yako au miamba ihamishwe toka mahali pake? “Naam, mwanga wa mtu mwovu utazimishwa; mwali wa moto wake hautangaa. Nyumbani kwake mwanga ni giza, taa inayomwangazia itazimwa. Hatua zake ndefu zitafupishwa; mipango yake itamwangusha chini. Nyayo zake mwenyewe zitamtia mtegoni; kila akitembea anakumbana na shimo. Mtego humkamata kisiginoni, tanzi humbana kabisa. Amefichiwa kitanzi ardhini; ametegewa mtego njiani mwake. Hofu kuu humtisha kila upande, humfuata katika kila hatua yake. Alikuwa na nguvu, lakini sasa njaa imembana; maafa yako tayari kumwangusha. “Ugonjwa mbaya unakula ngozi yake, maradhi ya kifo hula viungo vyake. Anangolewa katika nyumba aliyoitegemea, na kupelekwa kwa mfalme wa vitisho. Nyumba yake tupu, wengine wataishi humo; madini ya kiberiti yametawanywa katika makao yake. Yeye ni kama mti uliokauka mizizi, matawi yake juu yamenyauka. Nchini hakuna atakayemkumbuka; jina lake halitatamkwa tena barabarani. Ameondolewa mwangani akatupwa gizani; amefukuzwa mbali kutoka duniani. Hana watoto wala wajukuu; hakuna aliyesalia katika makao yake. Watu wa magharibi wameshangazwa na yaliyompata, hofu imewakumba watu wa mashariki. Hayo ndio yanayowapata wasiomjali Mungu; hapo ndipo mahali pa wasiomjua Mungu.” Kisha Yobu akajibu: “Mtaendelea kunitesa mpaka lini, na kunivunjavunja kwa maneno? Mara hizi zote kumi mmenishutumu. Je, hamwoni aibu kunitendea vibaya? Hata kama ingekuwa nimekosa kweli, kosa langu lanihusu mimi mwenyewe. Mnaishusha hadhi yangu mpate kujikuza; mnanilaumu kwa kunyenyekezwa kwangu. Jueni kwamba Mungu amenitendea vibaya, na kuninasa katika wavu wake. Tazama napiga yowe: ‘Dhuluma!’ Lakini sijibiwi. Naita kwa sauti kubwa, lakini sipati haki yangu. Njia yangu ameiziba kwa ukuta ili nisipite amezitia giza njia zangu. Amenivua fahari yangu; ameiondoa taji yangu kichwani. Amenivunja pande zote, nami nimekwisha; tumaini langu amelingoa kama mti. Ameichochea ghadhabu yake dhidi yangu; ameniona kuwa kama adui yake. Majeshi yake yanijia kwa pamoja; yametengeneza njia ya kuja kwangu, yamepiga kambi kuizunguka nyumba yangu. Mungu amewaweka ndugu zangu mbali nami; rafiki zangu wakuu wamenitoroka kabisa. Jamaa zangu na marafiki hawanisaidii tena. Wageni nyumbani mwangu wamenisahau; watumishi wangu wa kike waniona kuwa mgeni. Mimi nimekuwa kwao mtu wasiyemjua. Namwita mtumishi wangu lakini haitikii, ninalazimika kumsihi sana kwa maneno. Nimekuwa kinyaa kwa mke wangu; chukizo kwa ndugu zangu mwenyewe. Hata watoto wadogo hunidharau, mara ninapojitokeza wao hunizomea. “Rafiki zangu wakuu wanachukizwa nami, wale niliokuwa nikiwapenda wamenipa kisogo. Mwili wangu umebakia tu mifupa na ngozi, nimeponea chupuchupu baada ya kupoteza yote. Nioneeni huruma, nioneeni huruma enyi rafiki zangu; maana mkono wa Mungu umenifinya. Kwa nini mnanifuatia kama Mungu? Mbona hamtosheki na mwili wangu? “Laiti maneno yangu yangeandikwa! Laiti yangeandikwa kitabuni! Laiti yangechorwa kwa chuma na risasi juu ya jiwe ili yadumu! Najua wazi Mkombozi wangu anaishi, mwishowe yeye atanipa haki yangu hapahapa duniani. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivyo, nitamwona Mungu kwa macho yangu mwenyewe. Mimi mwenyewe nitakutana naye; mimi mwenyewe na si mwingine nitamwona kwa macho. “Nyinyi mwaweza kujisemea: ‘Tutamfuatia namna gani? Tutapataje kwake kisa cha kumshtaki?’ Lakini tahadharini na adhabu. Chuki yenu yaweza kuwaletea kifo! Mnapaswa kujua: Mungu peke yake ndiye hakimu.” Kisha Sofari, Mnaamathi, akajibu: “Fikira zangu zanifanya nikujibu, wala siwezi kujizuia tena. Nasikia maonyo nisiyoweza kuvumilia, lakini akili yangu yanisukuma nijibu. “Wewe labda umesahau jambo hili: Kwamba tangu zamani Mungu alipomuumba mtu duniani, mwovu atajiona ameshinda kwa muda tu, furaha yake asiyemcha Mungu ni ya muda mfupi tu! Mwovu aweza kufana hata kufikia mbingu, kichwa chake kikafika kwenye mawingu, lakini atatupiliwa mbali kama mavi yake. Waliopata kumjua watajiuliza: ‘Yuko wapi?’ Atatoweka kama ndoto, asionekane tena, atafutika kama maono ya usiku. Aliyemwona, hatamwona tena, wala pale alipoishi hapatatambuliwa tena. Yeye mwenyewe itambidi kurudisha mali yake yote, watoto wake wataomba huruma kwa maskini. Japo alijisikia amejaa nguvu za ujana, lakini zote zitalala pamoja naye mavumbini. “Mdomoni mwake uovu ni mtamu kama sukari, anauficha chini ya ulimi wake; hataki kabisa kuuachilia, bali anaushikilia kinywani mwake. Lakini ufikapo tumboni huwa mchungu, mkali kama sumu ya nyoka. Mwovu humeza mali haramu na kuitapika; Mungu huitoa tumboni mwake. Anachonyonya mtu mwovu ni sumu ya nyoka; atauawa kwa kuumwa na nyoka. Hataishi kuiona mitiririko ya fanaka, wala vijito vya mafanikio na utajiri. Matunda ya jasho lake atayaachilia, hatakuwa na uwezo wa kuyaonja, kwa sababu amewaangamiza maskini na kuwaacha, amenyakua nyumba ambazo hakuzijenga. “Kwa vile ulafi wake hauna mwisho, hataweza kuokoa chochote anachothamini. Baada ya kula hakuacha hata makombo, kwa hiyo fanaka yake yote haitadumu. Kileleni mwa fanaka dhiki itamvamia, balaa itamkumba kwa nguvu zote. Akiwa anajishughulisha kushibisha tumbo, Mungu atamletea ghadhabu yake imtiririkie kama chakula chake. Labda ataweza kuepa upanga wa chuma, kumbe atachomwa na upanga wa shaba. Mshale utachomolewa kutoka mwilini mwake; ncha yake itatolewa mgongoni mwake ikingaa, vitisho vya kifo vitamvamia. Hazina zake zitaharibiwa, moto wa ajabu utamteketeza; kilichobaki nyumbani mwake kitateketezwa. Mbingu zitaufichua uovu wake, dunia itajitokeza kumshutumu. Mali zake zitanyakuliwa katika siku ya ghadhabu ya Mungu. Hicho ndicho apewacho mtu mwovu kutoka kwa Mungu, ndicho mwovu alichopangiwa na Mungu.” Kisha Yobu akajibu: “Sikilizeni kwa makini maneno yangu; na hiyo iwe ndiyo faraja yenu. Nivumilieni, nami nitasema, na nikisha sema endeleeni kunidhihaki. Je, mimi namlalamikia binadamu? Ya nini basi, nikose uvumilivu? Niangalieni, nanyi mshangae, fumbeni mdomo kwa mkono. Nikifikiri yaliyonipata nafadhaika nafa ganzi mwilini kwa hofu. Kwa nini basi waovu wanaishi bado? Mbona nguvu zao zaongezeka hata uzeeni? Huwaona watoto wao wakifanikiwa; na wazawa wao wakipata nguvu. Kwao kila kitu ni salama bila hofu; wala kiboko cha Mungu hakiwafikii. Naam, ng'ombe wao wote huongezeka, huzaa bila matatizo yoyote. Watoto wao wachanga huwatembeza kama kundi; na watoto wao hucheza ngoma; hucheza muziki wa ngoma na vinubi, na kufurahia sauti ya filimbi. Huishi maisha ya fanaka kisha hushuka kwa amani kuzimu. Humwambia Mungu, ‘Usitusumbue! Hatutaki kujua matakwa yako. Mungu Mwenye Nguvu ni nini hata tumtumikie? Tunapata faida gani tukimwomba dua?’ Kufanikiwa kwao si kuko mikononi mwao, wakiwa wamemweka Mungu mbali na mipango yao? “Mara ngapi umepata kuona mwanga wa maisha ya mwovu umezimwa, wakapata kukumbwa na maafa, au Mungu amewahi kuwaangamiza kwa hasira yake? Hata hivyo, na wapeperushwe kama majani makavu, wawe kama makapi yanayochukuliwa na dhoruba! “Nyinyi mwasema, ‘Mungu amewawekea watoto wao adhabu ya watu hao waovu.’ Kwa nini hawalipizi wao wenyewe, wapate kutambua! Waone wao wenyewe wakiangamia; waone wenyewe ghadhabu ya Mungu mwenye nguvu. Maana wakifa watajali nini juu ya wazawa wao, wakati siku zao zitakapokuwa zimefika mwisho? Je, binadamu aweza kumfunza Mungu maarifa, Mungu ambaye huwahukumu wakazi wa mbinguni? “Mtu hufa katika kilele cha ufanisi wake, akiwa katika raha mustarehe na salama; amejaa mafuta tele mwilini, na mifupa yake ikiwa bado na nguvu. Mwingine hufa na huzuni kubwa moyoni, akiwa hajawahi kuonja lolote jema. Hata hivyo, wote hufa na kuzikwa, wote hufunikwa na mabuu. “Sikilizeni! Mimi nayajua mawazo yenu yote, na mipango yenu ya kunidharau. Eti mwauliza, ‘Iko wapi nyumba ya mkuu? Iko wapi nyumba alimoishi mwovu?’ “Je, hamjawauliza wapita njia, mkakubaliana na ripoti yao? Mwovu husalimishwa siku ya maafa, huokolewa siku ya ghadhabu! Ni nani atakayemshutumu mtu mwovu, au atakayemlipa kwa yote aliyotenda? Anapochukuliwa kupelekwa kaburini, kaburi lake huwekewa ulinzi. Watu wengi humfuata nyuma na wengine wengi sana humtangulia. Anapozikwa, udongo huteremshwa taratibu. Mtawezaje basi, kunifariji kwa maneno matupu? majibu yenu hayana chochote ila uongo.” Kisha Elifazi, Mtemani, akajibu Yobu: “Je, binadamu anafaa chochote kwa Mungu? Kwa kweli mwenye hekima anajifaidi mwenyewe tu. Je, unadhani wamfurahisha Mungu kwa kuwa mnyofu? Au anapata faida gani kama huna hatia? Unadhani anakurudi na kukuhukumu kwa sababu wewe unamheshimu? La! Uovu wako ni mkubwa mno! Ubaya wako hauna mwisho! Wewe umemnyanganya ndugu yako nguo ya rehani; umemchukulia nguo hiyo moja aliyokuwa nayo. Umewanyima maji wale waliokuwa wamechoka; umewanyima chakula wale walio na njaa. Umemruhusu mwenye cheo kuchukua ardhi yote; umemwacha anayependelewa aishi humo. Umewaacha wajane waende mikono mitupu; umewanyima yatima uwezo wao. Kwa hiyo mitego imekuzunguka pande zote, hofu ya ghafla imekuvamia. Giza limekuangukia usione kitu; mafuriko ya maji yamekufunika. Twajua Mungu yuko huko juu mbinguni. Tazama nyota za juu kabisa zilivyo mbali! Lakini wewe wasema: ‘Mungu ajua nini? Je, aweza kupenya mawingu akatoa hukumu? Mawingu mazito yamemzunguka asipate kuona yeye hutembea nje ya anga la dunia!’ “Je, umeamua kufuata njia za zamani ambazo watu waovu wamezifuata? Hao walifagiliwa kabla ya wakati wao, misingi yao ilikumbwa mbali na maji. Hao ndio waliomwambia Mungu, ‘Achana nasi!’ Na ‘Wewe Mungu Mwenye Nguvu waweza nini juu yetu?’ Lakini Mungu ndiye aliyejaza nyumba zao fanaka, lakini walimweka mbali na mipango yao! Wanyofu huona na kufurahi, wasio na hatia huwacheka na kuwadharau, Wanasema ama kweli maadui zetu wameangamizwa, na walichobakiza kimeteketezwa kwa moto. “Sasa, Yobu, kubaliana na Mungu uwe na amani, na hapo mema yatakujia. Pokea mafundisho kutoka kwake; na yaweke maneno yake moyoni mwako. Ukimrudia Mungu na kunyenyekea, ukiondoa uovu mbali na makao yako, ukitupilia mbali mali yako, ukaitupa dhahabu ya Ofiri ukingoni mwa kijito, Mungu Mwenye Nguvu akawa ndio dhahabu yako, na fedha yako ya thamani; basi, ndipo utakapomfurahia Mungu mwenye nguvu na kutazama kwa matumaini; utamwomba naye atakusikiliza, nawe utazitimiza nadhiri zako. Chochote utakachoamua kitafanikiwa, na mwanga utaziangazia njia zako. Maana, Mungu huwaporomosha wenye majivuno, lakini huwaokoa wanyenyekevu. Yeye humwokoa mtu asiye na hatia; wewe utaokolewa kwa matendo yako mema.” Kisha Yobu akajibu: “Leo pia lalamiko langu ni chungu. Napata maumivu na kusononeka. Laiti ningejua mahali nitakapompata Mungu! Ningeweza kwenda hata karibu naye. Ningeleta kesi yangu mbele yake, na kumtolea hoja yangu. Ningeweza kujua atakachonijibu, na kuelewa atakachoniambia. Je, angeshindana nami kwa nguvu zake zote? La! Bila shaka angenisikiliza. Yeye aweza kuzungumza na mtu mnyofu, Mungu, hakimu wangu angeamua kuwa sina hatia milele. “Tazama, nakwenda mbele, lakini simpati, narudi nyuma, lakini siwezi kumwona. Namtafuta upande wa kushoto lakini simwoni; nageukia kulia, lakini siwezi kumwona. Lakini yeye anajua njia ninayofuata; atakapomaliza kunijaribu nitatoka humo safi kama dhahabu. Nafuata nyayo zake kwa uaminifu njia yake nimeishikilia wala sikupinda. Kamwe sijaacha kushika amri yake, maneno yake nimeyatunza moyoni mwangu. Lakini yeye habadiliki, nani awezaye kumgeuza? Analotaka, ndilo analofanya! Atanijulisha yote aliyonipangia; na mengi kama hayo yamo akilini mwake. Hivyo, natetemeka kwa hofu mbele yake; hata nikifikiria tu napatwa na woga. Mungu ameufanya moyo wangu ufifie, Mungu Mwenye Nguvu amenitia hofu. Maana nimekumbwa na giza, na giza nene limetanda usoni mwangu. “Mbona Mungu Mwenye Nguvu haweki wakati maalumu wa hukumu; au kwa nini wamjuao hawazijui siku hizo zake? Watu wanaoondoa alama za mipaka ya mashamba, na wengine huiba mifugo na kuilisha. Huwanyanganya yatima punda wao, humweka rehani ng'ombe wa mjane. Huwasukuma maskini kando ya barabara; maskini wa dunia hujificha mbele yao. Kwa hiyo kama pundamwitu maskini hutafuta chakula jangwani wapate chochote cha kuwalisha watoto wao. Maskini wanalazimika kuokota mabaki ya mavuno mashambani, wanaokota katika mashamba ya mizabibu ya waovu. Usiku kucha hulala uchi bila nguo wakati wa baridi hawana cha kujifunikia. Wamelowa kwa mvua ya milimani, hujibanza miambani kujificha wasilowe. Wapo na wanaowanyakua watoto yatima vifuani mwa mama yao. Wengine huwaweka rehani watoto wa maskini. Watoto hao hufanywa waende uchi bila nguo, wakivuna ngano huku njaa imewabana, wakiwatengenezea waovu mafuta yao, au kukamua divai bila hata kuionja. Kutoka mjini kilio cha wanaokufa chasikika, na walioumizwa hupaza sauti kuomba msaada; lakini Mungu hasikilizi kabisa sala zao. “Wapo wengine waovu wasiopenda mwanga, wasiozifahamu njia za mwanga, na hawapendi kuzishika njia zake. Mwuaji huamka mapema alfajiri, ili kwenda kuwaua maskini na fukara, na usiku ukifika, kazi yake ni kuiba. Mzinifu naye hungojea giza liingie; akisema, ‘Hakuna atakayeniona;’ kisha huuficha uso wake kwa nguo. Usiku wezi huvunja nyumba, lakini mchana hujifungia ndani; wala hawajui kabisa mwanga ni nini. Kwao wote giza nene ni mwanga wa asubuhi; wao ni marafiki wa vitisho vya giza nene. “Lakini mwasema: ‘Waovu huchukuliwa haraka na mafuriko ya maji, makao yao hubaki kuwa nchi iliyolaaniwa; hakuna aendaye kwenye mashamba yao ya mizabibu.’ Kama theluji inavyoyeyuka katika joto na ukame ndivyo Kuzimu kunavyowanyakua waovu. Maana mzazi wao huwasahau watu hao, hakuna atakayewakumbuka tena. Ndivyo uovu ulivyovunjwa kama mti. “Waovu huwadhulumu wanawake wasiopata watoto. Wala hawawatendei wema wanawake wajane. Mungu, kwa nguvu yake huwaangamiza wenye uwezo, huinuka nao hukata tamaa ya kuishi. Huwaacha waovu wajione salama, lakini macho yake huchunguza mienendo yao. Waovu hufana kwa muda tu, kisha hutoweka, hunyauka na kufifia kama jani, hukatiliwa mbali kama masuke ya ngano. Nani basi, awezaye kuhakikisha kuwa mimi ni mwongo na kuonesha kwamba maneno yangu si kweli?” Kisha Bildadi, Mshuhi, akajibu: “Mungu ni mwenye uwezo mkuu, watu wote na wamche. Yeye huweka amani mpaka juu kwake mbinguni. Nani awezaye kuhesabu majeshi yake? Ni nani asiyeangaziwa na mwanga wake? Mtu awezaje basi, kuwa mwadilifu mbele ya Mungu? Binadamu tu awezaje kujidai kuwa safi? Kwake Mungu, hata mwezi haungai vya kutosha; nyota nazo si safi mbele yake; sembuse mtu ambaye ni mdudu, binadamu ambaye ni buu tu!” Kisha Yobu akajibu: “Aa! Jinsi gani ulivyomsaidia asiye na uwezo! Jinsi gani ulivyomwokoa asiye na nguvu! Jinsi gani ulivyomshauri asiye na hekima, na kumshirikisha ujuzi wako! Lakini umetamka hayo kwa ajili ya nani? Nani aliyekusukuma kuongea hivyo?” Bildadi akajibu: “Mizimu huko chini yatetemeka, maji ya chini na wakazi wake yaogopa. Kuzimu kuko wazi kabisa mbele ya Mungu. Abadoni haina kifuniko chochote. Mungu hutandaza kaskazini mahali patupu, na hutundika dunia mahali pasipo na kitu, huyafunga maji mawinguni yawe mazito, nayo mawingu hayapasuki kwa uzito wake. Huufunika uso wa mwezi na kutandaza juu yake wingu. Amechora duara juu ya uso wa bahari, penye mpaka kati ya mwanga na giza. Mungu akitoa sauti ya kukemea, nguzo za mbingu hutetemeka na kustaajabu. Kwa nguvu zake aliituliza bahari; kwa maarifa yake alimwangamiza dude Rahabu. Kwa pumzi yake aliisafisha anga; mkono wake ulilichoma joka lirukalo. Yamkini haya ni machache tu ya matendo yake, ni minongono tu tunayosikia juu yake. Nani awezaye kujua ukuu wa nguvu yake?” Yobu akaendelea kutoa hoja yake, akasema: “Naapa kwa Mungu aliye hai, aliyeniondolea haki yangu, Mungu Mwenye Nguvu aliyeifanya nafsi yangu iwe na uchungu! Naapa kuwa kadiri ninavyoweza kupumua, roho ya Mungu ikiwa bado ndani yangu; midomo yangu kamwe haitatamka uongo, wala ulimi wangu kusema udanganyifu. Siwezi kabisa kusema kuwa nyinyi mnasema ukweli mpaka kufa kwangu nasema sina hatia. Nashikilia unyofu wangu, wala sitauacha; katika dhamiri yangu sina cha kunihukumu maishani mwangu. “Adui yangu na apate adhabu ya mwovu, anayeinuka kunilaumu aadhibiwe kama mbaya. Asiyemcha Mungu ana tumaini gani, Mungu anapomkatilia mbali, anapomwondolea uhai wake? Je, atakapokumbwa na taabu, Mungu atasikia kilio chake? Mwovu hawezi kufurahi mbele ya Mungu Mwenye Nguvu; hataweza kudumu akimwomba Mungu. Nitawafundisheni kitendo cha Mungu kilivyo, sitawaficheni mipango yake Mungu Mwenye Nguvu. Lakini nyinyi mnajua jambo hilo vizuri sana! Mbona, basi mnaongea upuuzi? “Hiki ndicho Mungu alichomwekea mtu mwovu, alichopangiwa mdhalimu kupata ni hiki: Watoto wake hata wawe wengi watauawa kwa upanga; wazawa wake hawatakuwa na chakula cha kutosha. Wale watakaopona watakufa kwa maradhi mabaya, na wajane wao hawatawaombolezea. Hata akirundika fedha kama mavumbi, na mavazi kama udongo wa mfinyanzi, na arundike tu, lakini mnyofu ndiye atakayeyavaa, na fedha yake watagawana watu wasio na hatia. Nyumba ajengayo mwovu ni kama utando wa buibui, ni kama kibanda cha mlinzi shambani. Huenda kulala tajiri, lakini ni mara ya mwisho; atafungua macho yake, na utajiri wake umetoweka! Vitisho humvamia kama mafuriko; usiku hukumbwa na kimbunga. Upepo wa mashariki humpeperusha akatoweka; humfagilia mbali kutoka makao yake. Upepo huo humvamia bila huruma; atajaribu kuukimbia lakini mbio za bure. Upepo humzomea akimbiapo, na kumfyonya toka mahali pake. “Hakika kuna machimbo ya fedha, na mahali ambako dhahabu husafishwa. Watu huchimba chuma ardhini, huyeyusha shaba kutoka mawe ya madini. Wachimba migodi huleta taa gizani, huchunguza vina vya ardhi na kuchimbua mawe yenye madini gizani. Binadamu huchimba mashimo mbali na makazi ya watu, mbali na watu mahali kusipofikika, wachimba madini huninginia wamefungwa kamba. Kutoka udongoni chakula hupatikana, lakini chini yake kila kitu huvurugwa kwa moto. Katika mawe yake ndimo vilimo vito vya rangi ya samawati na udongo wake una vumbi la dhahabu. “Njia za kwenda kwenye migodi hiyo hakuna ndege mla nyama azijuaye; na wala jicho la tai halijaiona. Wanyama waendao kwa madaha hawajazikanyaga wala simba hawajawahi kuzipitia. Binadamu huchimbua miamba migumu kabisa, huichimbua milima na kuiondolea mbali. Hupasua mifereji kati ya majabali, na jicho lake huona vito vya thamani. Huziba chemchemi zisitiririke, na kufichua vitu vilivyofichika. “Lakini hekima itapatikana wapi? Ni mahali gani panapopatikana maarifa? Hakuna mtu ajuaye thamani ya hekima, wala hekima haipatikani nchini mwa walio hai. Vilindi vyasema, ‘Hekima haimo kwetu,’ na bahari yasema, ‘Haiko kwangu.’ Hekima haiwezi kupatikana kwa dhahabu, wala kwa kupima kiasi kingi cha fedha. Haiwezi kupimwa kwa dhahabu ya Ofiri, wala kwa vito vya Sardoniki au vya rangi ya samawati, dhahabu au kioo havilingani nayo, wala haiwezi kubadilishwa na vito vya dhahabu safi. Hekima ina thamani kuliko matumbawe na marijani, thamani yake yashinda thamani ya lulu. Topazi ya Kushi haiwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi kupewa bei ya dhahabu safi. “Basi, hekima yatoka wapi? Ni wapi panapopatikana maarifa? Imefichika machoni pa viumbe vyote hai, na ndege wa angani hawawezi kuiona. Abadoni na Kifo wasema, ‘Tumesikia uvumi wake kwa masikio yetu.’ “Mungu aijua njia ya hekima, anajua mahali inapopatikana. Maana yeye huona mpaka upeo wa dunia, huona kila kitu chini ya mbingu. Alipoupa upepo uzito wake, na kuyapimia maji mipaka yake; alipoamua mvua inyeshe wapi, umeme na radi vipite wapi; hapo ndipo alipoiona hekima na kuitangaza, aliisimika na kuichunguza.” Kisha Mungu akamwambia mwanadamu: “Tazama! Kumcha Bwana ndio hekima; na kujitenga na uovu ndio maarifa.” Kisha Yobu akaendelea na hoja yake, akasema: “Laiti ningekuwa kama zamani, wakati ule ambapo Mungu alinichunga; wakati taa yake iliponiangazia kichwani, na kwa mwanga wake nikatembea gizani. Wakati huo nilifikia ukamilifu wa maisha, wakati urafiki wa Mungu ulikaa nyumbani kwangu. Mungu Mwenye Nguvu alikuwa bado pamoja nami, na watoto wangu walinizunguka. Nyakati hizo niliogelea kwenye ufanisi, miamba ilinitiririshia vijito vya mafuta! Nilipokutana na wazee langoni mwa mji na kuchukua nafasi yangu mkutanoni, vijana waliponiona walisimama kando, na wazee walisimama wima kwa heshima. Wakuu waliponiona waliacha kuzungumza waliweka mikono juu ya midomo kuwataka watu wakae kimya. Sauti za waheshimiwa zilinyamazishwa, na vinywa vyao vikafumbwa. Kila aliyesikia habari zangu alinitakia heri na aliponiona, alikubali habari hizo kuwa kweli: Nilimwokoa maskini aliyenililia msaada, kadhalika na yatima asiyekuwa na wa kumsaidia. Waliokuwa karibu kuangamia walinitakia baraka, niliwafanya wajane waone tena furaha moyoni. Uadilifu ulikuwa vazi langu; kutenda haki kulikuwa kama joho na kilemba changu. Kwa vipofu nilikuwa macho ya kuwaonesha njia, kwa viwete nilikuwa miguu yao. Kwa maskini nilikuwa baba yao, nilifanya bidii kutetea haki za watu nisiowajua. Nilizivunja nguvu za watu waovu, nikawafanya wawaachilie mateka wao. Kisha nikafikiri: Nitafia kiotani mwangu nimetulia; siku za maisha yangu zitaongezeka kama mchanga. Mimi ni kama mti uliotandaza mizizi majini, umande wa usiku huburudisha matawi yangu. Napata fahari mpya daima, na nguvu zangu tayari kama mshale na upinde. “Wakati huo watu walinisikiliza na kungoja, walikaa kimya kungojea shauri langu. Nilipomaliza kusema hawakuwa na cha kuongeza, maneno yangu yaliwakolea kama matone ya mvua. Watu waliningojea kama wangojeavyo mvua, walikuwa kama watu wanaotazamia msimu wa vuli. Walipokata tamaa niliwaonesha uso wa furaha, uchangamfu wa uso wangu wakaungangania. Niliwatangulia kuwaongoza, nikawaonesha njia; nilikuwa kwao kama mfalme kati ya majeshi yake; kama mtu anayewafariji wenye msiba. “Lakini sasa watu wananidhihaki, tena watu walio wadogo kuliko mimi; watu ambao baba zao niliwaona hawafai hata kuwaangalia mbwa wangu wakilinda kondoo. Ningepata faida gani mikononi mwao, watu ambao nguvu zao zilikuwa zimewaishia? Katika ufukara na njaa kali walitafutatafuta cha kutafuna nyikani sehemu tupu zisizokuwa na chakula. Walichuma mimea jangwani na majani msituni wakala, walikula hata mizizi ya mti wa mfagio. Walifukuzwa mbali na watu, watu waliwapigia kelele kama wezi. Iliwapasa kutafuta usalama mapangoni, kwenye mashimo ardhini na miambani. Huko vichakani walilia kama wanyama, walikusanyika pamoja chini ya upupu. Walikuwa wapumbavu wakuu na mabaradhuli ambao walilazimika kufukuzwa nchini kwa kiboko. “Na sasa wamenitungia wimbo wa kunizomea, nimekuwa kitu cha dhihaka kwao. Wananichukia na kuniepa; wakiniona tu wanatema mate. Kwa kuwa Mungu amenidhoofisha na kuniaibisha, wamekuwa huru kunitendea wapendavyo. Genge la watu lainuka kunishtaki likitafuta kuniangusha kwa kunitegea. Linanishambulia ili niangamie. Watu hao hukata njia yangu huchochea balaa yangu, na hapana mtu wa kuwazuia. Wanakuja kama kwenye ufa mkubwa, na baada ya shambulio wanasonga mbele. Hofu kuu imenishika; hadhi yangu imetoweka kama kwa upepo, na ufanisi wangu umepita kama wingu. “Sasa sina nguvu yoyote nafsini mwangu; siku za mateso zimenikumba. Usiku mifupa yangu yote huuma, maumivu yanayonitafuna hayapoi. Mungu amenikaba kwa mavazi yangu, amenibana kama ukosi wa shati langu. Amenibwaga matopeni; nimekuwa kama majivu na mavumbi. Nakulilia, lakini hunijibu, nasimama kuomba lakini hunisikilizi. Umegeuka kuwa mkatili kwangu, wanitesa kwa mkono wako wenye nguvu. Wanitupa katika upepo na kunipeperusha; wanisukasuka huku na huko katika dhoruba kali. Naam! Najua utanipeleka tu kifoni, mahali watakapokutana wote waishio. “Je, mtu akikumbwa na maangamizi hainui mkono? Je, mtu akiwa taabuni haombi msaada Je, sikuwalilia wale waliokuwa na taabu? Je, sikuona uchungu kwa ajili ya maskini? Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinipata, nilipongojea mwanga, giza lilikuja. Moyo wangu wahangaika wala hautulii kamwe; siku za mateso zimekumbana nami. Napitapita nikiomboleza, kwangu hamna jua. Nasimama hadharani kuomba msaada. Kwa kilio nimekuwa ndugu yake mbwamwitu, mimi na mbuni hamna tofauti. Ngozi yangu imebambuka mifupa yangu inaungua kwa homa. Kinubi changu kimekuwa cha kufanya matanga filimbi yangu kwa ajili ya kuomboleza. “Nimejifunga rasmi mimi mwenyewe, macho yangu yasimtazame msichana kwa tamaa. Au je, nangojea nini kutoka kwa Mungu aliye juu? Mungu Mwenye Nguvu ameniwekea kitu gani? Je, maafa hayawapati watu waovu na maangamizi wale watendao mabaya? Je, Mungu haoni njia zangu, na kujua hatua zangu zote? “Kama nimeishi kwa kufuata uongo, kama nimekuwa mbioni kudanganya watu, Mungu na anipime katika mizani ya haki, naye ataona kwamba sina hatia. Kama hatua zangu zimepotoka, moyo wangu ukafuata tamaa za macho yangu; kama mikono yangu imechafuliwa na dhambi, jasho langu na liliwe na mtu mwingine, mazao yangu shambani na yangolewe. “Kama moyo wangu umevutwa kwa mke wa mtu, kama nimenyemelea mlangoni kwa jirani yangu, basi, mke wangu na ampikie mume mwingine, na wanaume wengine wamtumie. Jambo hilo ni kosa kuu la jinai, uovu ambao hakimu lazima atoe adhabu. Kosa langu lingekuwa kama moto, wa kuniteketeza na kuangamiza, na kuchoma kabisa mapato yangu yote. Kama nimekataa kesi ya mtumishi wangu wa kiume au wa kike, waliponiletea malalamiko yao, nitafanya nini basi Mungu atakaponikabili? Je, akinichunguza nitamjibu nini? Maana Mungu ndiye aliyeniumba mimi na mtumishi wangu; yeye ndiye aliyetuumba sisi wote. “Je, nimepata kumnyima maskini mahitaji yake au kuwafanya wajane watumaini bure? Je, nimekula chakula changu peke yangu, bila kuwaachia yatima nao wapate chochote? La! Tangu ujana wangu nimekuwa mlezi wao, tangu utoto wangu nimewaongoza wajane. Je, nilimwona mtu anakufa kwa kukosa nguo, au maskini ambaye hana nguo ya kuvaa, bila kumpa joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo wangu naye akanitakia baraka za shukrani ya moyo? Kama nimenyosha mkono mahakamani dhidi ya yatima, nikijua nitapendelewa na mahakimu, basi, bega langu na lingoke, mkono wangu na ukwanyuke kiwikoni mwake. Maana maafa kutoka kwa Mungu ni kitisho kwangu; mimi siwezi kuukabili ukuu wake. “Je, tumaini langu nimeliweka katika dhahabu, au, nimeiambia dhahabu safi, ‘Wewe ni usalama wangu?’ Je, nimepata kufurahia wingi wa utajiri wangu au kujivunia mapato ya mikono yangu? Kama nimeliangalia jua likiangaza, na mwezi ukipita katika uzuri wake, na moyo wangu ukashawishika kuviabudu, nami nikaibusu mikono yangu kwa heshima yake, huo pia ungekuwa uovu wa kuadhibiwa na mahakimu maana ningekuwa mwongo mbele ya Mungu aliye juu. “Je, nimefurahia kuangamia kwa adui yangu, au kufurahi alipopatwa na maafa? La! Sikuruhusu kinywa changu kumtakia mabaya, kwa kumlaani ili afe. Watumishi wangu wote wanasema wazi kila mgeni amekaribishwa nyumbani mwangu. Msafiri hakulala nje ya nyumba yangu, nilimfungulia mlango mpita njia. Je nimeficha makosa yangu kama wengine? Je nimekataa kukiri dhambi zangu? Sijaogopa kusimama mbele ya umati wa watu, wala kukaa kimya au kujifungia ndani, eti kwa kuogopa kutishwa na dharau zao. Laiti angekuwapo mtu wa kunisikiliza! Naweza kutia sahihi yangu katika kila nilichosema. Namwambia Mungu Mwenye Nguvu anijibu! Laiti mashtaka wanayonitolea maadui zangu yangeandikwa! Ningeyavaa kwa maringo mabegani na kujivisha kichwani kama taji. Ningemhesabia Mungu kila kitu nilichofanya, ningemwendea kama mwana wa mfalme. Kama nimeiiba ardhi ninayoilima, nikasababisha mifereji yake iomboleze, kwa kufaidika na mazao yake bila kulipa na kusababisha kifo cha wenyewe, basi miiba na iote humo badala ya ngano, na magugu badala ya shayiri.” Mwisho wa hoja za Yobu. Basi hawa watu watatu: Elifazi, Bildadi na Sofari, wakaacha kumjibu Yobu kwa vile alijiona kuwa mwema. Ndipo Elihu, mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa ukoo wa Rama, akakasirika. Alimkasirikia Yobu kwa sababu Yobu alijiona yeye mwadilifu na sio Mungu. Pia, aliwakasirikia rafiki watatu wa Yobu kwa sababu hawakuwa na la kumjibu Yobu, na hivyo kuonesha kwamba Mungu amekosa. Elihu alikuwa amekaa kimya wakati hao wazee waliposema na Yobu kwa kuwa yeye alikuwa kijana kuliko wao. Lakini alipoona hao watu watatu wameshindwa kumjibu Yobu, aliwaka hasira. Basi, Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi akaanza kusema: “Mimi ni kijana, nyinyi ni wazee zaidi; kwa hiyo niliogopa kuwaambieni mawazo yangu. Nilisema moyoni: ‘Waache wenye siku nyingi waseme, wenye miaka mingi wafundishe hekima.’ Lakini hiyo roho iliyomo ndani ya mtu, hiyo pumzi ya Mungu Mwenye Nguvu, ndio inayomwezesha mwanadamu kufahamu. Si lazima kuwa mzee ili uwe na hekima wala wazee siyo wenye kufahamu lililo sawa. Kwa hiyo nasema, ‘Nisikilizeni, acheni nami nitoe maoni yangu.’ “Basi, mimi nilingojea mlichotaka kusema, nilisikiliza misemo yenu ya hekima, mlipokuwa mnajaribu kutafuta la kusema. Niliwasikiliza kwa makini sana, lakini hakuna mmoja wenu aliyemshinda Yobu; nyote mlishindwa kuyajibu maneno yake. Jihadharini msije mkasema, ‘Sasa tumepata hekima. Atakayemshinda ni Mungu, sio binadamu.’ Maneno ya Yobu hayakuwa kwa ajili yangu, kwa hiyo sitamjibu kama mlivyomjibu nyinyi. “Nyinyi mmeduwaa; mmeshindwa, nyinyi hamna cha kusema zaidi. Je, ningoje tu kwa vile hamsemi, kwa sababu mnakaa tu bila kujibu kitu? Mimi pia nitatoa jibu langu; mimi nitatoa pia maoni yangu. Ninayo maneno mengi sana, roho yangu yanisukuma kusema. Moyo wangu umefurika kama divai iliyozibwa, kama kiriba cha divai mpya tayari kupasuka. Ni lazima niseme ili nipate nafuu; yanipasa kufungua kinywa changu na kujibu. Sitampendelea mtu yeyote wala kutumia maneno ya kubembeleza mtu. Maana mimi sijui kubembeleza mtu, la sivyo, Muumba wangu angeniangamiza. “Sasa, Yobu, sikiliza hoja yangu; sikiliza maneno yangu yote. Tazama, nafumbua kinywa changu, naam, ulimi wangu utasema. Nitasema kadiri ya unyofu wa moyo wangu; ninayoyajua nitayasema kwa uaminifu. Roho ya Mungu iliniumba, nayo pumzi ya Mungu Mwenye Nguvu yanipa uhai. Nijibu, kama unaweza. Panga hoja zako vizuri mbele yangu, ushike msimamo wako. Wewe na mimi ni sawa mbele ya Mungu; mimi pia niliumbwa kwa sehemu ya udongo. Kwa hiyo huna sababu ya kuniogopa; maneno yangu mazito hayatakulemea. Kweli umesema, nami nikasikia; nimeyasikia yote uliyosema. Wewe umesema, u safi na wala huna kosa, u safi kabisa na huna hatia; umesema kwamba Mungu anakutafutia kisa, na kukuona kama adui yake. Anakufunga miguu minyororo, na kuchunguza hatua zako zote. “Lakini Yobu, nakuambia hapo umekosea. Mungu ni mkuu kuliko binadamu. Kwa nini unashindana naye, ukisema hatajibu swali lako moja? Mungu anaposema hutumia njia moja, au njia nyingine lakini mtu hatambui. Mungu huongea na watu katika ndoto na maono, wakati usingizi mzito unapowavamia, wanaposinzia vitandani mwao. Hapo huwafungulia watu masikio yao; huwatia hofu kwa maonyo yake, wapate kuachana na matendo yao mabaya, na kuvunjilia mbali kiburi chao. Hivyo humkinga mtu asiangamie shimoni, maisha yake yasiangamie kwa upanga. “Mungu humrudi mtu kwa maumivu yamwekayo kitandani, maumivu hushika viungo vyake bila kukoma; naye hupoteza hamu yote ya chakula, hata chakula kizuri humtia kinyaa. Mwili wake hukonda hata asitambuliwe, na mifupa yake iliyofichika ikatokeza nje. Yuko karibu sana kuingia kaburini, na maisha yake karibu na wale waletao kifo. Lakini malaika akiwapo karibu naye, mmoja kati ya maelfu ya watetezi wa Mungu, ili kumwonesha lililo jema la kufanya, akamwonea huruma na kumwambia Mungu; ‘Mwokoe asiingie Shimoni, ninayo fidia kwa ajili yake.’ Hapo mwili wake utaweza kuwa tena kama kijana, ataweza kurudia tena nguvu zake za ujana. Kisha atamwomba Mungu na kukubaliwa, atakuja mbele yake kwa furaha, na Mungu atamrudishia fahari yake. Atashangilia mbele ya watu na kusema: ‘Nilitenda dhambi na kupotosha haki, nami sikuadhibiwa kutokana na hayo. Mungu aliniokoa nisiangamie Shimoni; nimebaki hai na ninaona mwanga.’ “Tazama Mungu humfanyia binadamu haya yote, tena mara mbili, mara tatu. Humwokoa binadamu asiangamie Shimoni, aweze kuona mwanga wa maisha. Sikia Yobu, nisikilize kwa makini; kaa kimya, nami nitasema. Kama una la kusema, nijibu; sema, maana nataka kukuona huna hatia. La sivyo, nyamaza unisikilize, kaa kimya nami nikufunze hekima.” Kisha Elihu akaendelea kusema: “Sikilizeni maneno yangu enyi wenye hekima, nitegeeni masikio yenu, nyinyi wenye ujuzi. Sikio huyapima maneno, kama vile ulimi uonjavyo chakula. Basi, na tuchague lililo sawa, tuamue miongoni mwetu lililo jema. Basi, Yobu ametamka: ‘Mimi Yobu sina hatia, Mungu ameniondolea haki yangu. Ingawa sina hatia naonekana kuwa mwongo; kidonda changu hakiponyeki ingawa sina kosa.’ Ni nani aliye kama Yobu ambaye kwake ubaradhuli ni kama kunywa maji? Huandamana na watenda maovu hutembea na watu waovu. Maana amesema, ‘Mtu hapati faida yoyote, kujisumbua kumpendeza Mungu.’ “Kwa hiyo nisikilizeni, enyi wenye ujuzi. Mungu kamwe hawezi kufanya uovu; Mungu Mwenye Nguvu hawezi kufanya kosa. Mungu atamlipa mtu kadiri ya matendo yake, atamlipiza kulingana na mwenendo wake. Ni ukweli mtupu: Mungu hafanyi ovu; Mungu Mwenye Nguvu kamwe hapotoshi haki. Je, kuna aliyemkabidhi mamlaka juu ya dunia? Uwezo wake juu ya ulimwengu ni wake peke yake. Kama Mungu angejifikiria tu yeye mwenyewe, akiondoa pumzi yake ya uhai duniani, viumbe vyote vingeangamia kabisa, naye binadamu angerudi mavumbini. “Kama una akili sikiliza; sikiliza ninachokuambia. Je, anayetawala ulimwengu kwa sheria zake anachukia haki? Je, utathubutu kumhukumu mwadilifu na mwenye nguvu? Amwambiaye mfalme, ‘Wewe ni takataka!’ Na watu mashuhuri, ‘Nyinyi ni waovu!’ Yeye hawapendelei wakuu, wala kuwajali matajiri kuliko maskini, maana wote hao ni kazi ya mikono yake. Kufumba na kufumbua hao wamekufa; hutikiswa usiku na kuaga dunia; nao wenye nguvu hufutiliwa mbali bila kutumia nguvu za mtu. “Macho ya Mungu huchunguza mienendo ya watu; yeye huziona hatua zao zote. Hakuna weusi wala giza nene ambamo watenda maovu waweza kujificha. Mungu hahitaji kumjulisha mtu wakati wa kumleta mbele ya mahakama yake. Huwaangamiza wenye nguvu bila uchunguzi, na kuwaweka wengine mahali pao. Kwa kuwa anayajua matendo yao yote, huwaporomosha usiku wakaangamia. Huwachapa hadharani kwa ajili ya uovu wao, kwa sababu wameacha kumfuata yeye, wakazipuuza njia zake zote. Hata wakasababisha kilio cha maskini kimfikie Mungu, Mungu akasikiliza kilio chao hao walioteswa. Kama Mungu akinyamaza, nani awezaye kumlaumu? Kama akificha uso wake, nani awezaye kumwona, liwe ni taifa au mtu mmojammoja? Hufanya hivyo, mtu mbaya asitawale, au wale wahatarishao maisha ya watu. “Tuseme mtu amemwambia Mungu, ‘Nimekosa, sitatenda dhambi tena. Nioneshe makosa nisiyoweza kuyaona kama nimetenda mabaya sitayarudia tena.’ Je, Mungu atapaswa kumwadhibu kama uonavyo wewe? Wewe ndiwe unayeamua, sio mimi. Basi, sema unachofikiri wewe. Mtu yeyote mwenye akili, na kila mwenye hekima anayenisikiliza atasema: ‘Yobu anaongea bila kutumia akili, maneno yake hayana maana.’ Laiti Yobu angechunguzwa mpaka mwisho, kwa maana anajibu kama watu waovu. Huongeza uasi juu ya dhambi zake; anaeneza mashaka kati yetu, na kuzidisha maneno yake dhidi ya Mungu.” Kisha Elihu akaendelea kusema: “Je, Yobu, unaona jambo hili ni sawa na kufikiri kinyume cha Mungu ukiuliza: ‘Nimepata faida gani kama sikutenda dhambi? Nimefaidika kuliko kama ningalitenda dhambi?’ Mimi nitakujibu wewe, na rafiki zako pia. Hebu zitazame mbingu! Tazama mawingu yaliyo juu kuliko wewe! Ukitenda dhambi, je, Mungu ndiye unayemdhuru? Na kama ukizidisha makosa yako, wadhani unamwumiza? Kama wewe ni mwema, je, unampatia faida, au yeye anapokea kitu kutoka kwako? Uovu wako utamdhuru binadamu kama wewe, wema wako utamfaa binadamu mwenzako. “Kwa sababu ya udhalimu mwingi watu hulia, huomba msaada kwa sababu ya mapigo ya wenye nguvu. Lakini hakuna asemaye, ‘Yuko wapi Mungu, Muumba wangu, mwenye kunifanya niwe mchangamfu usiku, anayetuelimisha kuliko wanyama, na kutufanya wenye hekima kuliko ndege!’ Watu hao huomba msaada lakini Mungu hawajibu, kwa sababu ya majivuno ya watu waovu. Kweli Mungu hasikilizi kilio cha bure; Mungu Mwenye Nguvu hajali kilio hicho. Atakujibu vipi wakati wewe unasema kwamba humwoni na kwamba kesi yako iko mbele yake na wewe unamngojea! Sasa, kwa vile Mungu anazuia hasira yake, wala hajali sana makosa ya watu, Yobu unafungua mdomo kusema maneno matupu, unazidisha maneno bila akili.” Kisha Elihu akaendelea kusema: “Nivumilie kidogo, nami nitakuonesha kitu; maana bado ninacho cha kusema kwa niaba ya Mungu. Nitaleta hekima yangu kutoka mbali sana, na kuonesha kwamba Muumba wangu ni mwadilifu. Kweli maneno yangu si ya uongo; mwenye elimu kamili yuko hapa nawe. “Sikiliza Mungu ni mwenye nguvu wala hamdharau mtu yeyote; uwezo wa akili yake ni mkuu mno! Hawaachi waovu waendelee kuishi; lakini huwapatia wanaodhulumiwa haki zao. Haachi kuwalinda watu waadilifu; huwatawaza, wakatawala na kutukuka. Lakini kama watu wamefungwa minyororo, wamenaswa katika kamba za mateso, Mungu huwaonesha matendo yao maovu, na kwamba wao ni watu wenye kiburi. Huwafungua masikio wasikie mafunzo, na kuwaamuru warudi na kuacha uovu. Wakimtii Mungu na kumtumikia, hufanikiwa katika siku zao zote; miaka yao yote huwa ya furaha. Lakini wasipomtii, huangamia kwa upanga, na kufa kwa kukosa akili. “Wasiomcha Mungu hupenda kukasirika, hawamlilii msaada anapowabana. Hufa wangali bado vijana, maisha yao huisha kama ya walawiti. Lakini Mungu huwaokoa wanyonge kwa unyonge wao hutumia shida zao kuwafumbua macho. Mungu alikuvuta akakutoa taabuni, akakuweka mahali pa wasaa pasipo shida, na mezani pako akakuandalia vinono. “Lakini sasa umehukumiwa kama mwovu, hukumu ya haki imekukumba. Jihadhari ghadhabu isije ikakufanya ukadhihaki, au ukubwa wa mali za kukukomboa ukakupotosha. Je, kilio chako kitafaa kukutoa taabuni, au nguvu zako zote zitakusaidia? Usitamani usiku uje, ambapo watu hufanywa watoweke walipo. Jihadhari! Usiuelekee uovu maana umepatiwa mateso kukuepusha na uovu. Kumbuka ukuu wa uwezo wa Mungu; nani awezaye kumfundisha kitu? Nani basi aliyeweza kumpangia njia yake, au awezaye kumwambia: ‘Umekosea?’ “Usisahau kuyasifu matendo yake; ambayo watu wameyashangilia. Watu wote wameona aliyofanya Mungu; binadamu huyaona kutoka mbali. Mungu ni mkuu mno hata hatuwezi kumjua; muda wa maisha yake hauchunguziki. Yeye huyavuta kwake maji ya bahari, na kutoka ukungu hufanya matone ya mvua. Huyafanya mawingu yanyeshe mvua, na kuwatiririshia binadamu kwa wingi. Nani ajuaye jinsi mawingu yatandavyo, au jinsi radi ingurumavyo angani kwake? Yeye huutandaza umeme wake kumzunguka, na kuvifunika vilindi vya bahari. Kwa mvua huwalisha watu na kuwapatia chakula kwa wingi. Huukamata umeme kwa mikono yake, kisha hulenga nao shabaha, Radi hutangaza ujio wake Mungu, hata wanyama hujua kwamba anakuja. “Kutokana na hayo, moyo wangu unatetemeka, na kuruka kutoka mahali pake. Sikilizeni ngurumo ya sauti ya Mungu, na mvumo wa sauti kutoka kinywani mwake. Huufanya uenee chini ya mbingu yote, umeme wake huueneza pembe zote za dunia. Ndipo sauti yake hunguruma, sauti ya Mungu hunguruma kwa fahari na muda huo wote umeme humulikamulika. Mungu hupiga radi ya ajabu kwa sauti yake, hufanya mambo makuu tusiyoweza kuyaelewa. Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya nchi!’ Na manyunyu na mvua, ‘Nyesha kwa nguvu.’ Hufunga shughuli za kila mtu; ili watu wote watambue kazi yake. Wanyama wa porini hurudi mafichoni mwao, na hubaki katika mapango yao. Dhoruba huvuma kutoka chumba chake, na baridi kali kutoka ghalani mwake. Kwa pumzi ya Mungu barafu hutokea, uso wa maji huganda kwa haraka. Mungu hulijaza wingu manyunyu mazito; mawingu husambaza umeme wake. Kwa amri yake vyote huzunguka huku na huko, kutekeleza kila kitu anachokiamuru, kufanyika katika ulimwengu wa viumbe. Mungu hutekeleza matakwa yake duniani; iwe ni kwa ajili ya kuwaadhibu watu, au kwa ajili ya kuonesha upendo wake. “Unapaswa kusikiliza Yobu; nyamaza, usikilize maajabu ya Mungu. Je, wajua jinsi Mungu anavyovipa amri yake, na kufanya umeme wa mawingu yake ungae? Je, wajua jinsi mawingu yanavyoelea angani? Ndizo kazi za ajabu za yule aliye mkamilifu wa maarifa! Wewe wajiona umevaa nguo za joto sana, wakati upepo wa kusi unaivamia nchi. Je, waweza, kuzitandaza mbingu kama yeye zikawa ngumu kama kioo cha shaba? Tufundishe tutakachomwambia Mungu; maana hoja zetu si wazi, tumo gizani. Je, nani anathubutu kumwambia: Nataka kuongea? Nani aseme apate balaa? “Ghafla mtu hawezi tena kuona waziwazi: Jua limefichika nyuma ya mawingu, na upepo umefagia anga! Mngao mzuri hutokea kaskazini; Mungu amezungukwa na utukufu wa kutisha. Mungu Mwenye Nguvu asiyeweza kufikiwa na mtu, uwezo na uadilifu wake ni mkuu, amejaa wema wala hapotoshi haki kamwe. Kwa hiyo, watu wote humwogopa; yeye hamjali mtu yeyote mwenye kiburi.” Hapo Mwenyezi-Mungu alimjibu Yobu kutoka dhoruba: “Nani wewe unayevuruga mashauri yangu kwa maneno yasiyo na akili? Jikaze kama mwanamume, nami nitakuuliza nawe utanijibu. “Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya dunia? Niambie, kama una maarifa. Ni nani aliyeweka vipimo vyake, wajua bila shaka! Au nani aliyelaza kamba juu yake kuipima? Je, nguzo za dunia zimesimikwa juu ya nini, au nani aliyeliweka jiwe lake la msingi, nyota za asubuhi zilipokuwa zikiimba pamoja, na wana wa Mungu wakapaza sauti za shangwe? Ni nani aliyeyafunga mafuriko ya bahari wakati yalipozuka na kuvuma kutoka vilindini? Mimi ndiye niliyeifunika bahari kwa mawingu na kuiviringishia giza nene. Niliiwekea bahari mipaka, nikaizuia kwa makomeo na milango, nikaiambia: ‘Mwisho wako ni hapa, si zaidi! Mawimbi yako ya nguvu yatakomea hapa!’ “Yobu, tangu uzaliwe umewahi kuamuru kupambazuke? na kulifanya pambazuko lijue mahali pake, ili lipate kuikamata dunia kwa pembe zake na kuwatimulia mbali waovu waliomo? Dunia hugeuka na kupata rangi kama vazi; kama udongo wa mfinyanzi unavyogeuzwa na mhuri. Lakini waovu watanyimwa mwanga wao, mkono wanaonyosha kupiga watu utavunjwa. “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari? au kutembea juu ya sakafu ya kilindi cha bahari? Je, umewahi kuoneshwa malango ya kifo, au kuyaona malango ya makazi ya giza nene? Je, wajua ukubwa wa dunia? Niambie kama unajua haya yote. “Je, makao ya mwanga yako wapi? Nyumbani kwa giza ni wapi, ili upate kulipeleka kwenye makao yake, na kuifahamu njia ya kwenda huko kwake. Wewe unapaswa kujua, wewe ambaye umekwisha ishi miaka mingi! “Je, umewahi kuingia katika bohari za theluji, au kuona bohari za mvua ya mawe ambavyo nimevihifadhi kwa ajili ya wakati wa fujo, kwa ajili ya siku ya mapigano na vita? Ipi njia ya kwenda mahali mwanga unapogawanywa, au huko kunakotoka upepo wa mashariki ukasambazwa duniani? “Nani aliyechora angani njia kwa ajili ya mvua? Nani aliyeionesha radi njia yake mawinguni, ikasababisha mvua kunyesha nchini kusikoishi mtu na jangwani ambako hakuna mtu, ili kuiburudisha nchi kavu na kame na kuifanya iote nyasi? “Je, mvua ina baba? Au nani ameyazaa matone ya umande? Je, barafu ilitoka tumboni kwa nani? Nani aliyeizaa theluji? Maji hugeuka kuwa magumu kama jiwe, na uso wa bahari ukaganda. “Angalia makundi ya nyota: Je, unaweza kuifunga minyororo Kilimia, au kuvilegeza vifungo vya Orioni? Je, waweza kuziongoza nyota katika majira yake, au kumwongoza Dubu pamoja na watoto wake? Je, wazijua kanuni zinazotawala mbingu; Je, waweza kuzipangia taratibu zao duniani? “Je, waweza kupaza sauti na kuyaamuru mawingu yakufunike kwa mtiririko wa mvua? Je, wewe ukiamuru umeme umulike, utakujia na kusema: ‘Nipo hapa?’ Ni nani aliyemjulisha kwarara kujaa kwa mto Nili au aliyemwambia jogoo kwamba mvua inakuja? Nani mwenye akili ya kuweza kuhesabu mawingu, au kuinamisha viriba vya maji huko mbinguni? ili vumbi duniani igandamane na udongo ushikamane na kuwa matope? “Je, waweza kumwindia simba mawindo yake au kuishibisha hamu ya wana simba; wanapojificha mapangoni mwao, au kulala mafichoni wakiotea? Ni nani awapaye kunguru chakula chao, makinda yao yanaponililia mimi Mungu, na kurukaruka huku na huko kwa njaa? “Je, wajua mbuzi wa milimani huzaa lini, au umewahi kuona kulungu akizaa? Je, wajua huchukua mimba kwa muda gani, au siku yenyewe ya kuzaa waijua? “Wajua wakati watakapochuchumaa kuzaa, wakati wa kuzaa watoto wao? Watoto wao hupata nguvu, hukua hukohuko porini, kisha huwaacha mama zao na kwenda zao. “Nani aliyemwacha huru pundamwitu? Nani aliyewaacha waende kwa kuwafungua? Mimi niliwapa jangwa liwe makao yao, mbuga zenye chumvi kuwa makazi yao. Hujitenga kabisa na makelele ya miji, hasikilizi kelele ya kumfanyisha kazi. Hutembeatembea milimani kupata malisho, na kutafuta chochote kilicho kibichi. “Je, nyati atakubali kukutumikia? Au je, atakubali kulala zizini mwako? Je, waweza kumfunga nyati kamba kulima shamba, au avute jembe la kulimia? Je, utamtegemea kwa kuwa ana nguvu nyingi na kumwacha akufanyie kazi zako nzito? Je, wamtazamia nyati akuvunie mavuno yako, na kuleta nafaka mahali pa kupuria? “Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa madaha, lakini hawezi kuruka kama korongo. Mbuni huyaacha mayai yake juu ya ardhi ili yapate joto mchangani; lakini hajui kama yanaweza kukanyagwa, au kuvunjwa na mnyama wa porini. Mbuni huwatendea wanawe ukatili kama si wake, hata kazi yake ikiharibika yeye hana wasiwasi; kwa sababu nilimfanya asahau hekima yake, wala sikumpa sehemu yoyote ya akili. Lakini akianza kukimbia, humcheka hata farasi na mpandafarasi. “Je, Yobu, ndiwe uliyewapa farasi nguvu, ukawavika shingoni manyoya marefu? Je, ni wewe unayemfanya farasi aruke kama nzige? Mlio wake wa maringo ni wa ajabu! Huparapara ardhi mabondeni kwa pupa; hukimbilia kwenye mapigano kwa nguvu zake zote. Farasi huicheka hofu, na hatishiki; wala upanga hauwezi kumrudisha nyuma. Silaha wachukuazo wapandafarasi, hugongana kwa sauti na kungaa juani. Farasi husonga mbele, akitetemeka kwa hasira; tarumbeta iliapo, yeye hasimami. Kila ipigwapo tarumbeta, yeye hutoa sauti; huisikia harufu ya vita toka mbali, huusikia mshindo wa makamanda wakitoa amri kwa makelele. “Je, mwewe amejifunza kwako jinsi ya kuruka, na kunyosha mabawa yake kuelekea kusini? Je, tai hupaa juu kwa amri yako, na kuweka kiota chake juu milimani? Tai hufanya makazi yake juu ya miamba mirefu, na ncha kali za majabali ndizo ngome zake. Kutoka huko huotea mawindo, macho yake huyaona kutoka mbali. Makinda yake hufyonza damu; pale ulipo mzoga ndipo alipo tai.” Mwenyezi-Mungu akaendelea kumwambia Yobu: “Je, wewe mwenye kuchunguza makosa utashindana na Mungu Mwenye Nguvu? Wewe unayebishana nami Mungu, basi jibu mambo hayo!” Kisha Yobu akamjibu Mwenyezi-Mungu: “Mimi sifai kitu nitakujibu nini? Naufunga mdomo wangu. Nilithubutu kusema na sitasema tena. Nilisisitiza lakini sitaendelea kusema zaidi.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamjibu kutoka kimbunga: “Jikaze kama mwanamume. Nitakuuliza, nawe utanijibu. Je, unataka kweli kubatilisha hukumu yangu, kuniona nina hatia ili wewe usiwe na hatia? Je, una nguvu kama mimi Mungu? Waweza kunguruma kwa sauti kama yangu? “Basi, jioneshe kuwa na fahari na ukuu, ujipambe kwa utukufu na fahari. Wamwagie watu hasira yako kuu; mwangalie kila mwenye kiburi na kumwangusha. Mwangalie kila mwenye kiburi na kumporomosha, uwakanyage waovu mahali walipo. Wazike wote pamoja ardhini; mfunge kila mmoja kwa kifungo cha kifo. Hapo nitakutambua, kwamba nguvu yako mwenyewe imekupa ushindi. “Liangalie lile dude Behemothi, nililoliumba kama nilivyokuumba wewe. Hilo hula nyasi kama ng'ombe, lakini mwilini lina nguvu ajabu, na misuli ya tumbo lake ni imara. Huufanya mkia wake mgumu kama mwerezi, mishipa ya mapaja yake imeshonwa pamoja. Mifupa yake ni mabomba ya shaba, viungo vyake ni kama pao za chuma. “Hilo ni la kwanza la ajabu kati ya viumbe vyangu! Ni mimi Muumba wake niwezaye kulishinda. Milima wanamocheza wanyama wote wa porini hutoa chakula chake. Hujilaza chini ya vichaka vya miiba, na kujificha kati ya matete mabwawani. Hujisitiri katika vivuli vya vichaka vya miiba na vya miti iotayo kando ya vijito. Mto ukifurika haliogopi, halitishiki hata mto Yordani ukilifurikia kinywani. Nani awezaye kuliziba macho na kuliteka? Nani awezaye kulitoboa pua kwa mtego? Je, waweza kuvua dude Lewiyathani kwa ndoana, au kuufunga ulimi wake kwa kamba? Je, unaweza kulitia kamba puani mwake, au kulitoboa taya kwa kulabu? Je, wadhani litakusihi uliachilie? Je, litazungumza nawe kwa upole? Je, litafanya mapatano nawe, ulichukue kuwa mtumishi wako milele? Je, utacheza nalo kama ndege, au kulifunga kamba licheze na wajakazi wako? Wadhani wavuvi watashindania bei yake? Je, wafanyabiashara watathubutu kulikata na kugawana? Je, waweza kuichoma ngozi yake kwa mikuki, au kichwa chake kwa mfumo wa kuvua samaki? Jaribu tu kuligusa, uone cha mtema kuni; Kamwe hutarudia tena kufanya hivyo! “Yeyote anayeliona hilo dude, hufa moyo na kuzirai. Hakuna mtu yeyote mkali athubutuye kulishtua. Nani, basi awezaye kusimama mbele yangu? Nani aliyenipa kitu, ili nitakiwe kumrudishia? Chochote kilicho chini ya mbingu ni changu. “Sitaacha kukueleza juu ya viungo vya hilo dude au juu ya nguvu zake na umbo lake zuri. Nani awezaye kumbambua vazi lake la nje? Nani awezaye kutoboa deraya lililovaa? Nani awezaye kufungua kinywa chake? Meno yake pande zote ni kitisho! Mgongo wake umefanywa kwa safu za ngao zilizoshikamana pamoja kama kwa mhuri, Kila moja imeshikamana na nyingine, hata hewa haiwezi kupenya katikati yake. Yameunganishwa pamoja, hata haiwezekani kuyatenganisha. Likipiga chafya, mwanga huchomoza, macho yake humetameta kama jua lichomozapo. Kinywani mwake hutoka mienge iwakayo, cheche za moto huruka nje. Puani mwake hufuka moshi, kama vile chungu kinachochemka; kama vile magugu yawakayo. Pumzi yake huwasha makaa; mwali wa moto hutoka kinywani mwake. Shingo yake ina nguvu ajabu, litokeapo watu hukumbwa na hofu. Misuli yake imeshikamana pamoja, imara kama chuma wala haitikisiki. Moyo wake ni mgumu kama jiwe, mgumu kama jiwe la kusagia. Linapoinuka, mashujaa hushikwa na woga, kwa pigo moja huwa wamezirai. Hakuna upanga uwezao kulijeruhi, wala mkuki, mshale au fumo. Kwake chuma ni laini kama unyasi, na shaba kama mti uliooza. Mshale hauwezi kulifanya likimbie; akitupiwa mawe ya teo huyaona kama makapi. Kwake, rungu ni kama kipande cha bua, hucheka likitupiwa fumo kwa wingi. Tumbo lake ni kama limefunikwa na vigae vikali; hukwaruza na kurarua udongo kama chombo cha kupuria. Bahari huisukasuka kama maji yachemkayo, huifanya itoe povu kama chupa ya mafuta. Lipitapo huacha nyuma alama inayongaa; povu jeupe huonekana limeelea baharini. Duniani hakuna kinachofanana nalo; hilo ni kiumbe kisicho na hofu. Huwaona kuwa si kitu wote wenye kiburi; hilo ni mfalme wa wanyama wote wakali.” Kisha Yobu akamjibu Mwenyezi-Mungu: “Najua kwamba waweza kila kitu, lolote unalokusudia haliwezi kuzuiliwa. Ulisema kuwa nilithubutu kutatiza mpango wako kijinga. Kweli nilitamka kitu ambacho sikuelewa mambo ya ajabu mno kwangu ambayo sikuwa ninayajua. Uliniambia nisikilize nawe utaniambia; kwamba utaniuliza nami nikujibu. Kweli nilikuwa nimesikia habari zako kwa masikio tu, lakini sasa nakuona kwa macho yangu mwenyewe. Kwa hiyo natubu pamoja na kujipaka mavumbi na majivu, najiona mimi mwenyewe kuwa si kitu kabisa.” Mwenyezi-Mungu alipomaliza kuongea na Yobu, alimwambia Elifazi, Mtemani, “Ghadhabu yangu imewaka dhidi yako na marafiki zako wawili kwani hamkusema ukweli juu yangu kama mtumishi wangu Yobu alivyofanya. Kwa hiyo chukueni mafahali saba na kondoo madume saba, mwende kwa mtumishi wangu Yobu, mkawatoe sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yenu. Naye mtumishi wangu Yobu atawaombeeni, nami nitaisikiliza sala yake na kuacha kuwatenda kulingana na upumbavu wenu; maana hamkusema ukweli juu yangu kama mtumishi wangu Yobu alivyofanya.” Basi, Elifazi Mtemani, Bildadi, Mshua na Sofari Mnaamathi, wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaambia. Mwenyezi-Mungu akaipokea sala ya Yobu. Baada ya Yobu kuwaombea rafiki zake, Mwenyezi-Mungu akamrudishia Yobu hali yake ya kwanza. Alimpa maradufu ya yote aliyokuwa nayo hapo awali. Kisha ndugu zake, dada zake na rafiki wote waliomfahamu hapo awali wakamwendea nyumbani kwake, wakala chakula pamoja naye. Wakampa pole na kumfariji kwa ajili ya mateso yote ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemletea. Kila mmoja wao akampa Yobu fedha na pete ya dhahabu. Katika miaka ya Yobu iliyofuata Mwenyezi-Mungu alimbariki zaidi kuliko hata alivyokuwa amembariki pale awali. Basi Yobu akawa na kondoo 14,000, ngamia 6,000, ng'ombe 2,000 na punda majike 1,000. Alikuwa pia na watoto wa kiume saba na wa kike watatu. Binti yake wa kwanza alimpa jina Yemima, wa pili Kezia, na wa mwisho Keren-hapuki. Katika nchi yote hiyo hapakuwa na wanawake waliokuwa wazuri kama mabinti wa Yobu. Baba yao akawaachia urithi kama alivyowaachia kaka zao. Baada ya hapo, Yobu aliishi miaka 140, akawaona wajukuu na vitukuu vyake vyote hadi kizazi cha nne. Basi, Yobu akafariki akiwa mzee wa miaka mingi. Heri mtu asiyefuata shauri la waovu, asiyeshiriki njia za wenye dhambi, wala kujumuika na wenye dharau; bali huifurahia sheria ya Mwenyezi-Mungu, na kuitafakari mchana na usiku. Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito, unaozaa matunda kwa wakati wake, na majani yake hayanyauki. Kila afanyalo hufanikiwa. Lakini waovu sivyo walivyo; wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo. Kwa hiyo watu waovu wataanguka wakati wa hukumu, wenye dhambi hawatakaa na kusanyiko la waadilifu. Maana Mwenyezi-Mungu huziongoza njia za waadilifu; lakini njia za waovu zitaishia katika maangamizi. Kwa nini mataifa yanafanya ghasia? Mbona watu wanafanya njama za bure? Wafalme wa dunia wanajitayarisha; watawala wanashauriana pamoja, dhidi ya Mwenyezi-Mungu na mteule wake. Wanasema: “Tujiondoe katika utawala wao; tutupilie mbali minyororo yao!” Mwenyezi-Mungu atawalaye juu mbinguni, anawacheka na kuwadhihaki. Kisha, anawakaripia kwa ghadhabu, na kuwatisha kwa hasira, akisema: “Nimemtawaza mfalme niliyemteua, anatawala Siyoni, mlima wangu mtakatifu!” Mfalme asema: “Nitatangaza azimio la Mwenyezi-Mungu. Mungu aliniambia: ‘Wewe ni mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako. Niombe nami nitakupa mataifa yawe urithi wako, na dunia nzima kuwa mali yako. Utawaponda kwa fimbo ya chuma; utawavunja kama chungu cha mfinyanzi!’” Sasa enyi wafalme, tumieni busara; sikilizeni onyo hili, enyi watawala wa dunia. Mtumikieni Mwenyezi-Mungu kwa uchaji; msujudieni na kutetemeka; asije akakasirika, mkaangamia ghafla; kwani hasira yake huwaka haraka. Heri yao wote wanaokimbilia usalama kwake! (Zaburi ya Daudi alipomkimbia Absalomu) Ee Mwenyezi-Mungu, tazama walivyo wengi adui zangu, ni wengi mno hao wanaonishambulia. Wengi wanasema juu yangu, “Hatapata msaada kwa Mungu.” Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu u ngao yangu kila upande; kwako napata fahari na ushindi wangu. Nakulilia kwa sauti, ee Mungu, nawe wanisikiliza kutoka mlima wako mtakatifu. Nalala na kupata usingizi, naamka tena maana wewe ee Mwenyezi-Mungu wanitegemeza. Sitayaogopa maelfu ya watu, wanaonizingira kila upande. Uje ee Mwenyezi-Mungu! Niokoe ee Mungu wangu! Wewe wawavunja mataya maadui zangu wote; wawavunja meno waovu wasinidhuru. Mwenyezi-Mungu ndiwe uokoaye; uwape baraka watu wako. (Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi) Ee Mungu mtetezi wa haki yangu, unijibu niombapo. Nilipokuwa katika shida, wewe ulinisaidia; unionee huruma na kusikia sala yangu. Jamani, mtaniharibia jina langu mpaka lini? Mpaka lini mtapenda upuuzi na kusema uongo? Jueni kuwa Mwenyezi-Mungu amejiteulia mwaminifu wake. Mwenyezi-Mungu husikia kila ninapomwomba. Tetemekeni kwa hofu na msitende dhambi; tafakarini vitandani mwenu na kunyamaza. Toeni tambiko zilizo sawa, na kumtumainia Mwenyezi-Mungu. Wengi husema: “Laiti tungepata tena fanaka! Utuangalie kwa wema, ee Mwenyezi-Mungu!” Lakini mimi umenijalia furaha kubwa moyoni, kuliko ya hao walio na divai na ngano kwa wingi. Nalala na kupata usingizi kwa amani; ee Mwenyezi-Mungu, wewe peke yako waniweka salama. (Kwa Mwimbishaji: Na filimbi. Zaburi ya Daudi) Usikilize maneno yangu, ee Mwenyezi-Mungu, usikie ninavyopiga kite. Usikilize kilio changu, Mfalme wangu na Mungu wangu, maana wewe ndiwe nikuombaye. Ee Mwenyezi-Mungu, alfajiri waisikia sauti yangu, asubuhi nakutolea tambiko yangu, kisha nangojea unijibu. Wewe si Mungu apendaye ubaya; kwako uovu hauwezi kuwako. Wenye majivuno hawastahimili mbele yako; wewe wawachukia wote watendao maovu. Wawaangamiza wote wasemao uongo; wawachukia wauaji na wadanganyifu. Lakini, kwa wingi wa fadhili zako, mimi nitaingia nyumbani mwako; nitakuabudu kuelekea hekalu lako takatifu, nitakusujudia kwa uchaji. Uniongoze, ee Mwenyezi-Mungu, katika uadilifu wako, maana maadui zangu ni wengi; uiweke njia yako wazi mbele yangu. Vinywani mwao hamna ukweli; mioyoni mwao wamejaa maangamizi, wasemacho ni udanganyifu wa kifo, ndimi zao zimejaa hila. Uwaadhibu kwa hatia yao ee Mungu; waanguke kwa njama zao wenyewe; wafukuze nje kwa sababu ya dhambi zao nyingi, kwa sababu wamekuasi wewe. Lakini wafurahi wote wanaokimbilia usalama kwako, waimbe kwa shangwe daima. Uwalinde wanaolipenda jina lako, wapate kushangilia kwa sababu yako. Maana wewe Mwenyezi-Mungu wawabariki waadilifu; wawakinga kwa fadhili zako kama kwa ngao. (Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa Sheminithi. Zaburi ya Daudi) Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako; usiniadhibu kwa ghadhabu yako. Unihurumie, ee Mwenyezi-Mungu, nimeishiwa nguvu; uniponye, ee Mwenyezi-Mungu, nataabika mpaka mifupani. Ninahangaika sana rohoni mwangu. Ee Mwenyezi-Mungu, utakawia mpaka lini? Unigeukie, ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe; unisalimishe kwa sababu ya fadhili zako. Huko kwa wafu hakuna anayekukumbuka; huko kuzimu ni nani awezaye kukusifu? Niko hoi kwa kilio cha uchungu; kila usiku nalowesha kitanda changu kwa machozi; kwa kulia kwangu naulowesha mto wangu. Macho yangu yamechoka kwa huzuni; yamefifia kwa kutaabishwa na adui. Ondokeni kwangu enyi nyote watenda maovu! Maana Mwenyezi-Mungu amesikia kilio changu. Mwenyezi-Mungu amesikia ombi langu; Mwenyezi-Mungu amekubali sala yangu. Maadui zangu wote wataaibika na kufadhaika; watarudi nyuma na kuaibishwa ghafla. (Ombolezo la Daudi kwa sababu ya Kushi wa kabila la Benyamini) Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nakimbilia usalama kwako; uniokoe na wote wanaonidhulumu, unisalimishe. La sivyo, watakuja kunirarua kama simba, wakanivutia mbali, pasiwe na wa kuniokoa. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu! Kama nimetenda moja ya mambo haya: Kama nimechafua mikono yangu kwa ubaya, kama nimemlipa rafiki yangu mabaya badala ya mema, au nimemshambulia adui yangu bila sababu, basi, adui na anifuatie na kunikamata; ayakanyage maisha yangu; na kuniulia mbali. Inuka ee Mwenyezi-Mungu, kwa hasira yako, uikabili ghadhabu ya maadui zangu. Inuka, ee Mungu wangu, wewe umeamuru haki ifanyike. Uyakusanye mataifa kandokando yako, nawe uyatawale kutoka juu. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wayahukumu mataifa; unihukumu kadiri ya uadilifu wangu, kulingana na huo unyofu wangu. Uukomeshe uovu wa watu wabaya, uwaimarishe watu walio wema, ee Mungu uliye mwadilifu, uzijuaye siri za mioyo na fikira za watu. Mungu ndiye ngao yangu; yeye huwaokoa wanyofu wa moyo. Mungu ni hakimu wa haki; kila siku hulaumu maovu. Watu wasipoongoka, Mungu atanoa upanga wake; atavuta upinde wake na kulenga shabaha. Atatayarisha silaha zake za hatari, na kuipasha moto mishale yake. Tazama! Mtu mbaya hutunga uovu, hujaa uharibifu na kuzaa udanganyifu. Huchimba shimo, akalifukua, kisha hutumbukia humo yeye mwenyewe. Uharibifu wake utamrudia yeye mwenyewe; ukatili wake utamwangukia yeye binafsi. Nitamshukuru Mwenyezi-Mungu kwani ni mwema; nitaimba sifa za jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Gitithi. Zaburi ya Daudi) Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wetu, kweli jina lako latukuka duniani kote! Utukufu wako waenea mpaka juu ya mbingu! Kwa sifa za watoto wadogo na wanyonyao, umejiwekea ngome dhidi ya adui zako, uwakomeshe waasi na wapinzani wako. Nikiangalia mbingu, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota ulizozisimika huko, mtu ni nini, ee Mungu, hata umfikirie, binadamu ni nini hata umjali? Umemfanya awe karibu kama Mungu, umemvika fahari na heshima. Ulimpa madaraka juu ya kazi zako zote; uliviweka viumbe vyote chini ya mamlaka yake: Kondoo, ng'ombe, na wanyama wa porini; ndege, samaki, na viumbe vyote vya baharini. Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wetu, kweli jina lako latukuka duniani kote! (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Muth-labeni. Zaburi ya Daudi) Nitakushukuru Mungu kwa moyo wangu wote; nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu. Nitafurahi na kushangilia kwa sababu yako; nitaliimbia sifa jina lako, ewe Mungu Mkuu. Wakati ulipotokea, maadui zangu walirudi nyuma, walijikwaa na kuangamia. Umenitetea kuhusu kisa changu cha haki; umeketi katika kiti chako cha enzi, ukatoa hukumu iliyo sawa. Umeyakemea mataifa, umewaangamiza waovu; majina yao umeyafutilia mbali milele. Maadui wameangamia milele; umeingolea mbali miji yao, kumbukumbu lao limetoweka. Lakini Mwenyezi-Mungu anatawala milele; ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu. Anauhukumu ulimwengu kwa haki; anayaamua mataifa kwa unyofu. Mwenyezi-Mungu ni ngome ya watu wanaoonewa; yeye ni ngome nyakati za taabu. Wanaokujua wewe, ee Mungu hukutegemea, wewe Mwenyezi-Mungu huwatupi wakutafutao. Mwimbieni sifa Mwenyezi-Mungu akaaye Siyoni. Yatangazieni mataifa mambo aliyotenda! Mungu hulipiza kisasi kwa umwagaji damu; kamwe hasahau kilio cha wanaoonewa. Unirehemu, ee Mwenyezi-Mungu! Ona mateso ninayoteswa na wanaonichukia; wewe waninyakua kutoka nguvu za kifo, nisimulie sifa zako mbele ya watu wa Siyoni, nipate kushangilia kwa sababu umeniokoa. Watu wa mataifa wametumbukia katika shimo walilochimba, wamenaswa miguu katika wavu waliouficha. Mwenyezi-Mungu amejionesha alivyo; ametekeleza hukumu. Watu waovu wamenaswa kwa matendo yao wenyewe. Waovu wataishia kuzimu; naam, mataifa yote yanayomsahau Mungu. Lakini fukara hawatasahauliwa daima; tumaini la maskini halitapotea milele. Inuka, ee Mwenyezi-Mungu! Usimwache binadamu ashinde. Uyakusanye mataifa mbele yako, uyahukumu. Uyatie hofu, ee Mwenyezi-Mungu, watu wa mataifa watambue kuwa wao ni watu tu! Ee Mwenyezi-Mungu, mbona wasimama mbali? Kwa nini wajificha wakati tumo taabuni? Kwa kiburi waovu wanawatesa maskini; njama zao ziwanase wao wenyewe. Mwovu hujisifia tamaa zake mbaya, mtu wa tamaa hulaani na kumkataa Mwenyezi-Mungu. Katika majivuno yake husema: “Mungu hatagundua.” Mawazo yake yote ni: “Hakuna Mungu.” Njia za mwovu hufanikiwa daima; kwake hukumu zako ziko mbali na mawazo yake, na huwadharau maadui zake wote. Huwaza moyoni: “Sitakuwa na wasiwasi; sitapatwa na dhiki maishani.” Kinywa chake kimejaa laana, udanganyifu na dhuluma; mwepesi kusema maneno ya kuchukiza na maovu. Hujificha vijijini huku anaotea, amuue kwa siri mtu asiye na hatia. Yuko macho kumvizia mnyonge; huotea mafichoni mwake kama simba. Huvizia apate kuwakamata maskini; huwanasa kwa mtego wake na kuwachukua. Mnyonge huvamiwa na kuangushwa chini; huangushwa kwa ukatili wa mtu mwovu. Mwovu huwaza moyoni mwake: “Mungu amesahau; ameficha uso wake, haoni kitu!” Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwaadhibu; usiwasahau wanaodhulumiwa. Ee Mungu, kwa nini mwovu anakudharau, na kusema ati hutamfanya awajibike? Lakini wewe wawaona wenye dhiki na shida; nawe daima uko tayari kuwasaidia. Mnyonge anakutegemea wewe, ee Mungu, wewe umekuwa daima msaada wa yatima. Uzivunje nguvu za mtu mwovu; ukomeshe uovu wake wote, usiwepo tena. Mwenyezi-Mungu ni mfalme milele na milele! Mataifa yasiyomjua yatatoweka nchini mwake. Ee Mwenyezi-Mungu, wapokea dua za mnyonge; wampa moyo na kumtegea sikio. Utawatendea haki yatima na wanaodhulumiwa, binadamu aliye udongo asiweze tena kuleta hofu. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Kwake Mwenyezi-Mungu nakimbilia usalama; mnawezaje basi kuniambia: “Ruka kama ndege, mpaka milimani, maana waovu wanavuta pinde; wameweka mishale tayari juu ya uta, wawapige mshale watu wema gizani! Kama misingi ikiharibiwa, mtu mwadilifu atafanya nini?” Mwenyezi-Mungu yumo katika hekalu lake takatifu; kiti cha enzi cha Mwenyezi-Mungu kiko mbinguni. Kwa macho yake huwachungulia wanadamu, na kujua kila kitu wanachofanya. Mwenyezi-Mungu huwapima waadilifu na waovu; huwachukia kabisa watu wakatili. Atawanyeshea waovu makaa ya moto na madini ya kiberiti; upepo wa hari utakuwa ndio adhabu yao. Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu na apenda uadilifu; watu wanyofu watakaa pamoja naye. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Sheminithi. Zaburi ya Daudi) Fanya haraka, ee Mwenyezi-Mungu! Watu wema wamekwisha; waaminifu wametoweka miongoni mwa watu. Kila mmoja humdanganya mwenzake, husema kwa kudanganya na kwa moyo wa unafiki. Ee Mwenyezi-Mungu uikomeshe hiyo midomo ya udanganyifu, na ndimi hizo zinazojigamba kupindukia. Wao husema: “Kwa ndimi zetu tutashinda; midomo tunayo, nani awezaye kututawala?” Lakini Mwenyezi-Mungu asema: “Kwa sababu maskini wanadhulumiwa, na wahitaji wanapiga kite, sasa naja, nami nitawapa usalama wanaoutazamia.” Neno la Mwenyezi-Mungu ni safi, safi kama fedha iliyosafishwa katika tanuri, naam, kama fedha iliyosafishwa mara saba. Utulinde, ee Mwenyezi-Mungu, utukinge daima na kizazi hiki kiovu. Waovu wanazunguka kila mahali; upotovu unatukuzwa kati ya watu. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Mpaka lini ee Mwenyezi-Mungu, utanisahau? Je, utanisahau mpaka milele? Mpaka lini utanificha uso wako? Nitakuwa na wasiwasi rohoni hadi lini, na sikitiko moyoni siku hata siku? Hadi lini adui zangu watafurahia taabu zangu? Uniangalie na kunijibu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Uyaangazie macho yangu, nisipatwe na usingizi wa kifo. Usiwaache maadui zangu waseme: “Tumemweza huyu!” Watesi wangu wasije wakafurahia kuanguka kwangu. Lakini mimi nazitumainia fadhili zako; moyo wangu na ufurahie wokovu wako. Nitakuimbia wewe, ee Mwenyezi-Mungu, kwa ukarimu mwingi ulionitendea! (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Wapumbavu hujisemea moyoni: “Hakuna Mungu.” Wote wamepotoka kabisa, wametenda mambo ya kuchukiza; hakuna hata mmoja atendaye jema! Mwenyezi-Mungu anawaangalia wanadamu kutoka mbinguni, aone kama kuna yeyote mwenye busara, kama kuna yeyote anayemtafuta Mungu. Lakini wote wamekosa, wote wamepotoka pamoja; hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja. “Je, hao watendao maovu hawana akili? Wanawatafuna watu wangu kama mikate; wala hawanijali mimi Mwenyezi-Mungu.” Hapo watashikwa na hofu kubwa, maana Mungu yu pamoja na waadilifu. Unaweza kuvuruga mipango ya maskini, lakini Mwenyezi-Mungu ndiye kimbilio lake. Laiti ukombozi wa Israeli ungefika kutoka Siyoni! Mwenyezi-Mungu atakaporekebisha hali ya watu wake, wazawa wa Yakobo watashangilia; Waisraeli watafurahi. (Zaburi ya Daudi) Nani ee Mwenyezi-Mungu atakayekaa hemani mwako? Nani atakayeishi juu ya mlima wako mtakatifu? Ni mtu aishiye bila lawama, atendaye daima yaliyo mema, asemaye ukweli kutoka moyoni; ni mtu asiyesengenya watu, asiyemtendea uovu rafiki yake, wala kumfitini jirani yake; ni mtu anayewadharau wafisadi, lakini huwaheshimu wamchao Mwenyezi-Mungu; ni mtu asiyegeuza kiapo chake hata kikimtia hasara; asiyekopesha fedha yake kwa riba, wala kupokea rushwa kumdhulumu asiye na hatia. Mtu atendaye hayo, kamwe hatatikisika. (Utenzi wa Daudi) Unilinde ee Mungu; maana kwako nakimbilia usalama. Namwambia Mungu: “Wewe u Bwana wangu; sina jema lolote ila wewe.” Ni bora sana hao watakatifu walioko nchini, kukaa nao ndiyo furaha yangu. Lakini wanaoabudu miungu mingine, watapata mateso mengi. Tambiko ya damu sitaitolea kamwe, na majina ya miungu hiyo sitayataja. Wewe ee Mwenyezi-Mungu ndiwe riziki yangu kuu, majaliwa yangu yamo mikononi mwako. Umenipimia sehemu nzuri sana; naam, urithi wangu ni wa kupendeza. Namsifu Mwenyezi-Mungu kwa kuniongoza, usiku dhamiri yangu yanionya. Namweka Mwenyezi-Mungu mbele yangu daima; yuko pamoja nami, wala sitatikisika. Kwa hiyo nitafurahi kwa moyo wote na kushangilia, nami nitakaa salama salimini. Naam wewe hutaiacha nafsi yangu kuzimu, hutaniacha mimi mwaminifu wako nipate kuoza. Wanionesha njia ya kufikia uhai; kuwako kwako kwanijaza furaha kamili, katika mkono wako wa nguvu mna mema ya milele. (Sala ya Daudi) Ee Mwenyezi-Mungu usikie kisa changu cha haki, usikilize kilio changu, uitegee sikio sala yangu isiyo na hila. Haki yangu na ije kutoka kwako, kwani wewe wajua jambo lililo la haki. Wewe wajua kabisa moyo wangu; umenijia usiku, kunichunguza, umenitia katika jaribio; hukuona uovu ndani yangu, sikutamka kitu kisichofaa. Kuhusu matendo watendayo watu; mimi nimeitii amri yako, nimeepa njia ya wadhalimu. Nimefuata daima njia yako; wala sijateleza kamwe. Nakuita, ee Mungu, kwani wewe wanijibu; unitegee sikio, uyasikie maneno yangu. Onesha fadhili zako za ajabu, uwaokoe kutoka kwa adui zao, wale wanaokimbilia usalama kwako. Unilinde kama mboni ya jicho; unifiche kivulini mwa mabawa yako, mbali na mashambulio ya waovu, mbali na maadui zangu hatari wanaonizunguka. Hao hawana huruma yoyote moyoni; wamejaa maneno ya kujigamba. Wananifuatia na kunizunguka; wananivizia waniangushe chini. Wako tayari kunirarua kama simba: Kama mwanasimba aviziavyo mawindo. Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwakabili na kuwaporomosha. Kwa upanga uiokoe nafsi yangu kutoka kwa waovu. Kwa mkono wako, ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe mikononi mwa watu hao, watu ambao riziki yao ni dunia hii tu. Uwajaze adhabu uliyowawekea, wapate ya kuwatosha na watoto wao, wawaachie hata na wajukuu zao. Lakini mimi nitauona uso wako, kwani ni mwadilifu; niamkapo nitajaa furaha kwa kukuona. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi, mtumishi wa Mungu, aliyomwimbia Mungu wakati alipomwokoa mkononi mwa Shauli na adui wengine) Nakupenda, ee Mwenyezi-Mungu, nguvu yangu! Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu na mkombozi wangu; Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia usalama; ngao yangu, nguvu za wokovu wangu na ngome yangu. Namwita Mwenyezi-Mungu astahiliye sifa anisaidie, nami naokolewa kutoka kwa maadui zangu. Kamba za kifo zilinizingira, mawimbi ya maangamizi yalinivamia; kamba za kuzimu zilinizinga, mitego ya kifo ilinikabili. Katika taabu yangu nilimwita Mwenyezi-Mungu, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Aliisikia sauti yangu hekaluni mwake; kilio changu kilimfikia masikioni mwake. Hapo dunia ikatetemeka na kutikisika; misingi ya milima ikayumbayumba, kwani Mungu alikuwa amekasirika. Moshi ulifuka kutoka puani mwake, moto uunguzao ukatoka kinywani mwake; makaa ya moto yalilipuka kutoka kwake. Aliinamisha anga, akashuka chini; na wingu jeusi chini ya miguu yake. Alipanda kiumbe chenye mabawa akaruka; akapaa kasi juu ya mabawa ya upepo. Alijifunika giza pande zote, mawingu mazito yaliyojaa maji yalimzunguka. Umeme ulimulika mbele yake; kukatokea mawinguni mvua ya mawe na makaa ya moto. Mwenyezi-Mungu alinguruma kutoka mbinguni; Mungu Mkuu akatoa sauti yake, kukatokea mvua ya mawe na makaa ya moto. Aliwapiga maadui mishale yake, akawatawanya, alirusha umeme, akawatimua. Ulipowakemea maadui zako ee Mwenyezi-Mungu, ulipowatisha kwa ghadhabu yako, vilindi vya bahari vilifunuliwa, misingi ya dunia ikaonekana. Mungu alinyosha mkono kutoka juu akanichukua, kutoka katika maji mengi alininyanyua. Aliniokoa kutoka kwa maadui zangu wenye nguvu nyingi, aliniokoa kutoka kwa hao walionichukia, maana walikuwa na nguvu kunishinda. Walinivamia nilipokuwa taabuni, lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa kinga yangu. Alinileta, akaniweka mahali pa usalama; alinisalimisha, kwani alipendezwa nami. Mwenyezi-Mungu alinipa tuzo kadiri ya uadilifu wangu; alinituza kwa vile mikono yangu haina hatia. Maana nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu, wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu. Nimeshika maagizo yake yote, sikuacha kufuata masharti yake. Mbele yake sikuwa na hatia; nimejikinga nisiwe na hatia. Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu; yeye ajua kwamba mikono yangu haina hatia. Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu; mwema kwa wale walio wema. Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu; lakini mkatili kwa watu walio waovu. Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu, lakini wenye majivuno huwaporomosha. Wewe ee Mwenyezi-Mungu, waniangazia; walifukuza giza langu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Kwa msaada wako nakishambulia kikosi; wewe wanipa nguvu ya kuruka ukuta. Huyu Mungu matendo yake hayana dosari! Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika; yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia usalama. Nani aliye Mungu isipokuwa Mwenyezi-Mungu? Nani aliye mwamba wa usalama ila Mungu wetu? Mungu ndiye anijaliaye nguvu kila upande; ndiye anayeifanya salama njia yangu. Ameiimarisha miguu yangu kama ya paa, na kuniweka salama juu ya vilele. Hunifunza kupigana vita, mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba. Umenipa ngao yako ya kuniokoa; mkono wako wa kulia umenitegemeza; wema wako umenifanikisha. Umenirahisishia njia yangu; wala miguu yangu haikuteleza. Niliwafuatia adui zangu na kuwakamata; sikurudi nyuma mpaka nimewaangamiza. Niliwaangusha chini wasiweze kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita; uliwaporomosha maadui chini yangu. Uliwafanya maadui zangu wakimbie, na wale walionichukia niliwaangamiza. Walipiga yowe lakini hapakuwa na wa kuwaokoa; walimlilia Mwenyezi-Mungu lakini hakuwajibu. Niliwatwanga wakawa kama vumbi inayopeperushwa na upepo; niliwakanyaga kama tope la njiani. Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu, ukanifanya mtawala wa mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Mara waliposikia habari zangu walinitii. Wageni walinijia wakinyenyekea. Wageni walikufa moyo; wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka. Mwenyezi-Mungu yu hai! Asifiwe mwamba wa usalama wangu; atukuzwe Mungu wa wokovu wangu. Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi; na kuyashinda mataifa chini yangu. Ameniokoa kutoka kwa maadui zangu, akanikuza juu ya wapinzani wangu, na kunisalimisha mbali na watu wakatili. Kwa hiyo nitakutukuza kati ya mataifa, ee Mwenyezi-Mungu nitaliimbia sifa jina lako. Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa; humwonesha fadhili zake huyo mteule wake, naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Mbingu zatangaza utukufu wa Mungu; anga ladhihirisha kazi ya mikono yake. Mchana waupasha habari mchana ufuatao, usiku waufahamisha usiku ufuatao. Hamna msemo au maneno yanayotumika; wala hakuna sauti inayosikika; hata hivyo, sauti yao yaenea duniani kote, na maneno yao yafika kingo za ulimwengu. Mungu ameliwekea jua makao yake angani; nalo hutoka kama bwana arusi chumbani mwake, lafurahi kama shujaa aliye tayari kushindana. Lachomoza toka upande mmoja, na kuzunguka hadi upande mwingine; hakuna kiwezacho kuliepa joto lake. Sheria ya Mwenyezi-Mungu ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya; masharti ya Mwenyezi-Mungu ni thabiti, huwapa hekima wasio na makuu. Kanuni za Mwenyezi-Mungu ni sawa, huufurahisha moyo; amri ya Mwenyezi-Mungu ni safi, humwelimisha mtu. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni jambo jema, na la kudumu milele; maagizo ya Mwenyezi-Mungu ni sawa, yote ni ya haki kabisa. Yatamanika kuliko dhahabu; kuliko dhahabu safi kabisa. Ni matamu kuliko asali; kuliko asali safi kabisa. Yanifunza mimi mtumishi wako; kuyafuata kwaniletea tuzo kubwa. Lakini nani aonaye makosa yake mwenyewe? Ee Mungu, niepushe na makosa nisiyoyajua. Unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi, usikubali hayo yanitawale. Hapo nitakuwa mkamilifu, wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa. Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yakubalike mbele yako, ee Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu na mkombozi wangu! (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Mwenyezi-Mungu akujibu uwapo taabuni; jina la Mungu wa Yakobo likulinde. Akupelekee msaada kutoka hekaluni mwake; akutegemeze kutoka mlima Siyoni. Azikumbuke sadaka zako zote; azikubali tambiko zako za kuteketezwa. Akujalie unayotamani moyoni mwako, aifanikishe mipango yako yote. Tutashangilia kwa ajili ya ushindi wako; tutatweka bendera kulitukuza jina la Mungu wetu. Mwenyezi-Mungu akutimizie maombi yako yote! Najua Mwenyezi-Mungu atamsaidia mfalme aliyemteua, atamjibu kutoka patakatifu pake mbinguni; kwa mkono wake wa kulia atamjalia ushindi mkubwa. Wengine hujigamba kwa magari ya vita; wengine hujigamba kwa farasi wao. Lakini sisi twajivunia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Hao watajikwaa na kuanguka; lakini sisi tutainuka na kusimama imara. Umjalie mfalme ushindi, ee Mwenyezi-Mungu; utujibu wakati tunapokuomba. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Mfalme ashangilia, ee Mwenyezi-Mungu, kwa nguvu yako, anafurahi mno kwa msaada uliompa. Umemtimizia matakwa ya moyo wake; wala hukumkatalia ombi lake. Umemjia, ukampa baraka nzurinzuri; umemvika taji ya dhahabu safi kichwani mwake. Alikuomba maisha nawe ukampa; ulimpa maisha marefu milele na milele. Kwa msaada wako ametukuka sana; wewe umemjalia fahari na heshima. Wamjalia baraka zako daima; wamfurahisha kwa kuwako kwako. Mfalme anamtumainia Mwenyezi-Mungu; kwa fadhili za Mungu Mkuu atakuwa salama. Mkono wako ewe mfalme utawakamata maadui zako wote; mkono wako wa kulia utawakamata wanaokuchukia. Utakapotokea utawaangamiza kama kwa tanuri ya moto. Mwenyezi-Mungu atawamaliza kwa hasira yake, moto utawateketeza kabisa. Utawaangamiza wazawa wao kutoka duniani; watoto wao hawatasalia kati ya binadamu. Hata kama wakipanga maovu dhidi yako, kama wakitunga mipango ya hila, kamwe hawataweza kufaulu. Kwa maana wewe utawatimua mbio, utawalenga usoni kwa mishale yako. Utukuzwe ee Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya nguvu yako! Tutaimba na kuusifu uwezo wako. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa utenzi wa kulungu wa alfajiri. Zaburi ya Daudi) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Mbona uko mbali sana kunisaidia, mbali na maneno ya kilio changu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu; napiga yowe usiku, lakini nafuu sipati. Hata hivyo, wewe ni mtakatifu; wewe watawala na kusifiwa na Waisraeli. Wazee wetu walikutegemea; walikutegemea, nawe ukawaokoa. Walikulilia wewe, wakaokolewa; walikutegemea, nao hawakuaibika. Lakini mimi ni mdudu tu, wala si mtu; nimepuuzwa na kudharauliwa na watu. Wote wanionao hunidhihaki; hunifyonya na kutikisa vichwa vyao. Husema: “Alimtegemea Mwenyezi-Mungu, basi, Mungu na amkomboe! Kama Mungu anapendezwa naye, basi, na amwokoe!” Lakini ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, uliniweka salama kifuani pa mama yangu. Nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu. Tangu nilipozaliwa wewe umekuwa Mungu wangu. Usikae mbali nami, kwani taabu imekaribia; wala hakuna wa kunisaidia. Maadui wengi wanizunguka kama fahali; wamenisonga kama fahali wakali wa Bashani! Wanafunua vinywa vyao kama simba, tayari kushambulia na kurarua. Nimekwisha kama maji yaliyomwagika; mifupa yangu yote imeteguka; moyo wangu ni kama nta, unayeyuka ndani mwangu. Koo langu limekauka kama kigae; ulimi wangu wanata kinywani mwangu. Umeniacha kwenye mavumbi ya kifo. Genge la waovu limenizunguka; wananizingira kama kundi la mbwa; wamenitoboa mikono na miguu. Nimebaki mifupa mitupu; maadui zangu waniangalia na kunisimanga. Wanagawana nguo zangu, na kulipigia kura vazi langu. Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu, usikae mbali nami; ewe msaada wangu, uje haraka kunisaidia. Iokoe nafsi yangu mbali na upanga, yaokoe maisha yangu makuchani mwa mbwa hao! Uniokoe kinywani mwa simba; iokoe nafsi yangu dhaifu toka pembe za nyati hao. Nitawasimulia ndugu zangu matendo yako; nitakusifu kati ya kusanyiko lao: Enyi mnaomcha Mwenyezi-Mungu, msifuni! Mtukuzeni enyi wazawa wote wa Yakobo! Mcheni Mungu enyi wazawa wote wa Israeli! Maana yeye hapuuzi au kudharau unyonge wa mnyonge; wala hajifichi mbali naye, ila humsikia anapomwomba msaada. Kwa sababu yako ninakusifu katika kusanyiko kubwa la watu; nitatimiza ahadi zangu mbele yao wakuchao. Maskini watakula na kushiba; wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu watamsifu. Mungu awajalie kuishi milele! Ulimwengu wote utakumbuka na kumrudia Mwenyezi-Mungu; jamaa zote za mataifa zitamwabudu. Maana Mwenyezi-Mungu ni mfalme; yeye anayatawala mataifa. Wenye kiburi wote duniani watasujudu mbele yake; wote ambao hufa watainama mbele yake, wote ambao hawawezi kudumisha uhai wao. Vizazi vijavyo vitamtumikia; watu watavisimulia habari za Mwenyezi-Mungu, watatangaza matendo yake ya wokovu. Watu wasiozaliwa bado wataambiwa: “Mwenyezi-Mungu ndiye aliyefanya hayo!” (Zaburi ya Daudi) Mwenyezi-Mungu ni mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Hunipumzisha kwenye malisho mabichi; huniongoza kando ya maji matulivu, na kuirudishia nafsi yangu nguvu mpya. Huniongoza katika njia sawa kwa hisani yake. Nijapopita katika bonde la giza kuu la kifo, sitaogopa hatari yoyote, maana wewe ee Mwenyezi-Mungu u pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanilinda. Umeniandalia karamu mbele ya maadui zangu; umenipaka mafuta kichwani pangu; kikombe changu umekijaza mpaka kufurika. Kweli wema wako na fadhili zako zitakuwa pamoja nami, siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu milele. (Zaburi ya Daudi) Dunia na vyote vilivyomo ni vyake Mwenyezi-Mungu; ulimwengu na wote waishio humo ni mali yake. Maana yeye aliweka misingi ya dunia juu ya bahari; aliisimika imara juu ya mito ya maji. Nani atakayepanda mlima wa Mwenyezi-Mungu? Nani atakayekaa katika hekalu lake takatifu? Ni mtu wa matendo mema na moyo safi, asiyeuelekeza moyo wake katika upuuzi, wala kuapa kwa uongo. Mtu huyo atapokea baraka kwa Mwenyezi-Mungu, na haki yake kwa Mungu mwokozi wake. Ndio hali ya kizazi cha watu wamtafutao yeye; naam, watu wamtafutao Mungu wa Yakobo. Fungukeni enyi milango; fungukeni enyi milango ya kale, ili Mfalme mtukufu aingie. Ni nani huyo Mfalme mtukufu? Ni Mwenyezi-Mungu, mwenye nguvu na uwezo; Mwenyezi-Mungu, mwenye uwezo vitani. Fungukeni enyi malango, fungukeni enyi milango ya kale, ili Mfalme mtukufu aingie. Ni nani huyo Mfalme mtukufu? Ni Mwenyezi-Mungu, wa majeshi, yeye ndiye Mfalme mtukufu. (Zaburi ya Daudi) Ee Mwenyezi-Mungu, kwako naielekeza nafsi yangu! Nakutumainia wewe, ee Mungu wangu, usiniache niaibike; adui zangu wasifurahie kushindwa kwangu. Usimwache anayekutumainia apate aibu; lakini waaibike wote wanaokuasi kwa makusudi. Unijulishe njia zako, ee Mwenyezi-Mungu; unifundishe nifuate unayotaka. Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha, kwani wewe ni Mungu, mwokozi wangu; ninakutegemea wewe kila siku. Uikumbuke huruma yako ee Mwenyezi-Mungu; uzikumbuke na fadhili zako kuu, ambazo zimekuwako tangu kale. Usikumbuke dhambi na makosa ya ujana wangu; unikumbuke kadiri ya fadhili zako, kwa ajili ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu ni mwema na mnyofu, kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia. Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu; naam, huwafundisha hao njia yake. Mwenyezi-Mungu hutenda kwa fadhili na uaminifu, kwa wale wanaoshika agano lake na maamuzi yake. Kwa ajili ya jina lako, ee Mwenyezi-Mungu, unisamehe kosa langu kwani ni kubwa. Kila mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu atamfunza njia ya kufuata. Mtu wa namna hiyo atafanikiwa daima, na wazawa wake watamiliki nchi. Mwenyezi-Mungu ni rafiki ya wale wamchao; yeye huwajulisha hao agano lake. Namwangalia Mwenyezi-Mungu daima; yeye atainasua miguu yangu mtegoni. Unielekee, ee Mungu, unionee huruma, maana mimi ni mpweke na mnyonge. Uniondolee mahangaiko ya moyoni mwangu; unitoe katika mashaka yangu. Uangalie mateso yangu na dhiki yangu; unisamehe dhambi zangu zote. Angalia jinsi walivyo wengi maadui zangu; ona jinsi wanavyonichukia kwa ukatili. Uyalinde maisha yangu, uniokoe; nakimbilia usalama kwako, usikubali niaibike. Wema na uadilifu vinihifadhi, maana ninakutumainia wewe. Ee Mungu, uwaokoe watu wako, Israeli; uwaokoe katika taabu zao zote. (Zaburi ya Daudi) Ee Mwenyezi-Mungu, unitetee, maana nimeishi bila hatia, nimekutumainia wewe bila kusita. Unijaribu, ee Mwenyezi-Mungu, na kunipima; uchunguze moyo wangu na akili zangu. Fadhili zako ziko mbele ya macho yangu, ninaishi kutokana na uaminifu wako. Sijumuiki na watu wapotovu; sishirikiani na watu wanafiki. Nachukia mikutano ya wabaya; wala sitajumuika na waovu. Nanawa mikono yangu kuonesha sina hatia, na kuizunguka madhabahu yako, ee Mwenyezi-Mungu, nikiimba wimbo wa shukrani, na kusimulia matendo yako yote ya ajabu. Ee Mwenyezi-Mungu, napenda makao yako, mahali unapokaa utukufu wako. Usiniangamize pamoja na wenye dhambi, wala usinitupe pamoja na wauaji, watu ambao matendo yao ni maovu daima, watu ambao wamejaa rushwa. Lakini mimi ninaishi kwa unyofu; unihurumie na kunikomboa. Mimi nimesimama mahali palipo imara; nitamsifu Mwenyezi-Mungu katika kusanyiko kubwa. (Zaburi ya Daudi) Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu, sitamwogopa mtu yeyote. Waovu wakinishambulia, na kutaka kuniangamiza, hao wapinzani wangu watajikwaa na kuanguka. Hata jeshi likinizunguka, moyo wangu hautaogopa kitu; hata nikikabiliwa na vita, bado nitakuwa na tumaini. Jambo moja nimemwomba Mwenyezi-Mungu, nalo ndilo ninalolitafuta: Nikae nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu siku zote za maisha yangu; niuone uzuri wake Mwenyezi-Mungu, na kutafuta maongozi yake hekaluni mwake. Siku ya taabu atanificha bandani mwake; atanificha katika hema lake, na kunisalimisha juu ya mwamba. Nami kwa fahari nitaangalia juu ya maadui zangu wanaonizunguka. Nitamtolea tambiko kwa shangwe hekaluni mwake, nitaimba na kumshangilia Mwenyezi-Mungu. Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, ninapokulilia, unionee huruma na kunijibu. Moyo wangu waniambia: “Njoo umtafute Mungu!” Basi, naja kwako, ee Mwenyezi-Mungu. Usiache kuniangalia kwa wema. Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako; wewe umekuwa daima msaada wangu. Usinitupe wala usiniache, ee Mungu Mwokozi wangu. Hata kama wazazi wangu wakinitupa, Mwenyezi-Mungu atanipokea kwake. Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu; uniongoze katika njia iliyo sawa, kwa sababu ya maadui zangu. Usiniache maadui wanitende wapendavyo; maana mashahidi wa uongo wananikabili, nao wanatoa vitisho vya ukatili. Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu katika makao ya walio hai. Mtegemee Mwenyezi-Mungu! Uwe na moyo, usikate tamaa! Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu! (Zaburi ya Daudi) Nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu! Ewe mwamba wa usalama wangu usiniwie kama kiziwi, la sivyo kama usiponisikiliza, nitakuwa kama wale washukao shimoni kwa wafu. Sikiliza sauti ya ombi langu, ninapokulilia unisaidie, ninapoinua mikono yangu kuelekea maskani yako takatifu. Usinipatilize pamoja na watu wabaya, pamoja na watu watendao maovu: Watu wasemao na wenzao maneno ya amani, kumbe wamejaa uhasama moyoni. Uwaadhibu kadiri ya matendo yao, kufuatana na maovu waliyotenda. Waadhibu kadiri ya matendo yao wenyewe; uwatendee yale wanayostahili. Hawajali matendo ya Mwenyezi-Mungu; hawatambui mambo aliyoyafanya. Kwa sababu hiyo atawabomoa, wala hatawajenga tena upya. Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, maana amesikiliza ombi langu. Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu; tegemeo la moyo wangu limo kwake. Amenisaidia nami nikashangilia kwa moyo; kwa wimbo wangu ninamshukuru. Mwenyezi-Mungu ni nguvu ya watu wake; yeye ni kimbilio la wokovu kwa mfalme wake mteule. Ee Mungu, uwaokoe watu wako; uwabariki watu hao walio mali yako. Uwe mchungaji wao na kuwategemeza milele. (Zaburi ya Daudi) Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima enyi viumbe vya mbinguni, semeni Mwenyezi-Mungu ni mtukufu na mwenye nguvu. Semeni jina la Mwenyezi-Mungu ni tukufu. Mwabuduni katika mahali pake patakatifu. Sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya maji; Mungu mtukufu angurumisha radi, sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya bahari! Sauti ya Mwenyezi-Mungu ina nguvu, sauti ya Mwenyezi-Mungu imejaa fahari. Sauti ya Mwenyezi-Mungu huvunja mierezi; Mwenyezi-Mungu avunja mierezi ya Lebanoni. Huirusha milima ya Lebanoni kama ndama, milima ya Sirioni kama mwananyati. Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutoa miali ya moto. Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa, Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa la Kadeshi. Sauti ya Mwenyezi-Mungu huitikisa mivule, hukwanyua majani ya miti msituni, na hekaluni mwake wote wasema: “Utukufu kwa Mungu!” Mwenyezi-Mungu ameketi juu ya gharika; Mwenyezi-Mungu ni mfalme atawalaye milele. Mwenyezi-Mungu na awape watu wake nguvu! Mwenyezi-Mungu na awabariki watu wake kwa amani! (Zaburi ya Daudi) Ee Mwenyezi-Mungu, nakutukuza maana umeniokoa, wala hukuwaacha maadui zangu wanisimange. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nilikulilia msaada, nawe ukaniponya. Ee Mwenyezi-Mungu, umeniokoa kutoka kuzimu; umenipa tena uhai, umenitoa miongoni mwa waendao kuzimu. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa, enyi waaminifu wake; kumbukeni utakatifu wake na kumshukuru. Hasira yake hudumu kitambo kidogo, wema wake hudumu milele. Kilio chaweza kuwapo hata usiku, lakini asubuhi huja furaha. Mimi nilipofanikiwa, nilisema: “Kamwe sitashindwa!” Kwa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu, umeniimarisha kama mlima mkubwa. Lakini ukajificha mbali nami, nami nikafadhaika. Nilikulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu; naam niliomba dua kwako ee Mwenyezi-Mungu: “Je, utapata faida gani nikifa na kushuka hadi kwa wafu? Je, mavumbi ya wafu yanaweza kukusifu? Je, yanaweza kusimulia uaminifu wako? Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, unihurumie; ee Mwenyezi-Mungu, unisaidie!” Wewe umegeuza maombolezo langu kuwa ngoma ya furaha; umeniondolea huzuni yangu, ukanizungushia furaha. Mimi nitakusifu wala sitakaa kimya. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nitakushukuru milele. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Kwako, ee Mwenyezi-Mungu, nakimbilia usalama, usiniache niaibike kamwe; kwa uadilifu wako uniokoe. Unitegee sikio, uniokoe haraka! Uwe kwangu mwamba wa usalama, ngome imara ya kuniokoa. Naam, wewe ni mwamba wangu na ngome yangu; kwa hisani yako uniongoze na kunielekeza. Unitoe katika mtego walionitegea mafichoni; maana wewe ni kimbilio la usalama wangu. Mikononi mwako naiweka roho yangu; umenikomboa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu mwaminifu. Wawachukia wanaoabudu sanamu batili; lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu. Nitashangilia na kufurahia fadhili zako, maana wewe waiona dhiki yangu, wajua na taabu ya nafsi yangu. Wewe hukuniacha nitiwe mikononi mwa maadui zangu; umenisimamisha mahali pa usalama. Unionee huruma, ee Mwenyezi-Mungu, niko taabuni; macho yangu yamechoka kwa huzuni, nimeishiwa nguvu mwilini na rohoni. Maisha yangu yamekwisha kwa majonzi; naam, miaka yangu kwa kulalamika. Nguvu zangu zimeniishia kwa kutaabika; hata mifupa yangu imekauka. Nimekuwa dharau kwa maadui zangu wote; kioja kwa majirani zangu. Rafiki zangu waniona kuwa kitisho; wanionapo njiani hunikimbia. Nimesahaulika kama mtu aliyekufa; nimekuwa kama chungu kilichovunjikavunjika. Nasikia watu wakinongonezana, vitisho kila upande; wanakula njama dhidi yangu, wanafanya mipango ya kuniua. Lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu. Nasema: “Wewe ni Mungu wangu!” Maisha yangu yamo mikononi mwako; uniokoe na maadui zangu, niokoe na hao wanaonidhulumu. Uniangalie kwa wema mimi mtumishi wako; uniokoe kwa fadhili zako. Usiniache niaibike ee Mwenyezi-Mungu, maana mimi ninakuomba; lakini waache waovu waaibike, waache wapotelee kwa mshangao huko kuzimu. Izibe midomo ya hao watu waongo, watu walio na kiburi na majivuno, ambao huwadharau watu waadilifu. Jinsi gani ulivyo mwingi wema wako, uliowawekea wale wanaokucha! Wanaokimbilia usalama kwako wawapa mema binadamu wote wakiona. Wawaficha mahali salama hapo ulipo, mbali na mipango mibaya ya watu; wawaweka salama katika ulinzi wako, mbali na ubishi wa maadui zao. Asifiwe Mwenyezi-Mungu, maana amenionesha fadhili zake kwa namna ya ajabu, nilipozingirwa kama mji unaoshambuliwa. Nami niliogopa na kudhani kwamba ulikuwa umenitupa; kumbe, ulisikia kilio changu nilipokuita unisaidie. Mpendeni Mwenyezi-Mungu, enyi watakatifu wake wote. Mwenyezi-Mungu huwalinda watu waaminifu; lakini huwaadhibu kabisa wenye kiburi wanavyostahili. Muwe hodari na kupiga moyo konde, enyi nyote mnaomtumainia Mwenyezi-Mungu. (Zaburi ya Daudi. Funzo) Heri yake mtu aliyesamehewa kosa lake, mtu ambaye dhambi yake imeondolewa kabisa. Heri mtu ambaye Mwenyezi-Mungu hamwekei hatia, mtu ambaye hana hila moyoni mwake. Wakati nilipokuwa sijakiri dhambi yangu, nilikuwa nimedhoofika kwa kulia mchana kutwa. Mchana na usiku mkono wako ulinilemea; nikafyonzwa nguvu zangu, kama maji wakati wa kiangazi. Kisha nilikiri makosa yangu kwako; wala sikuuficha uovu wangu. Nilisema ninakuungamia makosa yangu ee Mwenyezi-Mungu, ndipo nawe ukanisamehe dhambi zangu zote. Kwa hiyo, kila mwaminifu na akuletee maombi; jeshi likaribiapo au mafuriko, hayo hayatamfikia yeye. Wewe ndiwe kinga yangu; wewe wanilinda katika taabu. Umenijalia shangwe za kukombolewa. Mungu asema: “Nitakufunza na kukuonesha njia unayopaswa kufuata. Nitakushauri kwa uangalifu mkubwa. Usiwe mpumbavu kama farasi au nyumbu, ambao lazima wafungwe lijamu na hatamu, la sivyo hawatakukaribia.” Watu waovu watapata mateso mengi, bali wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu wazungukwa na fadhili zake. Furahini na kushangilia kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu; pigeni vigelegele vya shangwe enyi wanyofu wa moyo. Shangilieni kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu! Kumsifu Mungu ni wajibu wa watu wanyofu. Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa zeze; mwimbieni kwa kinubi cha nyuzi kumi. Mwimbieni wimbo mpya; pigeni kinubi vizuri na kushangilia. Neno la Mwenyezi-Mungu ni la kweli; na matendo yake yote ni ya kuaminika. Mungu apenda uadilifu na haki, dunia imejaa fadhili za Mwenyezi-Mungu. Mbingu ziliumbwa kwa neno la Mwenyezi-Mungu, na vyote vilivyomo kwa pumzi ya mdomo wake. Alikusanya maji ya bahari kama katika chupa, vilindi vya bahari akavifunga ghalani. Dunia yote na imwogope Mwenyezi-Mungu! Wakazi wote duniani, wamche! Maana alisema na ulimwengu ukawako; alitoa amri nao ukajitokeza. Mwenyezi-Mungu hupangua mipango ya mataifa, na kuyatangua mawazo yao. Mpango wa Mwenyezi-Mungu hudumu milele; maazimio yake yadumu vizazi vyote. Heri taifa ambalo Mungu wake ni Mwenyezi-Mungu; heri wale aliowachagua kuwa watu wake mwenyewe! Mwenyezi-Mungu huangalia chini kutoka mbinguni, na kuwaona wanadamu wote. Kutoka kwenye kiti chake cha enzi, huwaangalia wakazi wote wa dunia. Yeye huunda mioyo ya watu wote, yeye ajua kila kitu wanachofanya. Mfalme hawezi kuokolewa kwa kuwa na jeshi kubwa; wala shujaa hapati ushindi kwa nguvu zake kubwa. Farasi wa vita hafai kitu kwa kupata ushindi; nguvu zake nyingi haziwezi kumwokoa mtu. Mwenyezi-Mungu huwaangalia wale wamchao, watu ambao wanatumainia fadhili zake. Yeye huwaokoa katika kifo, huwaweka hai wakati wa njaa. Mioyo yetu yamtumainia Mwenyezi-Mungu. Yeye ni msaada wetu na ngao yetu. Naam twafurahi kwa sababu yake; tuna matumaini katika jina lake takatifu. Fadhili zako zikae nasi, ee Mwenyezi-Mungu, kwani sisi tumekuwekea tumaini letu. (Zaburi ya Daudi alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki) Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote, sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake. Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu, wanyonge wasikie na kufurahi. Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami, sote pamoja tulisifu jina lake. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu, na kuniondoa katika hofu zangu zote. Mgeukieni Mungu mpate kufurahi; nanyi hamtaaibishwa kamwe. Maskini alimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamsikia, na kumwokoa katika taabu zake zote. Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao, na kuwaokoa katika hatari. Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema. Heri mtu anayekimbilia usalama kwake. Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake; maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu. Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa; lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema. Njoni enyi vijana mkanisikilize, nami nitawafundisha kumcha Mwenyezi-Mungu. Je, watamani kufurahia maisha, kuishi maisha marefu na kufurahia mema? Basi, acha kusema mabaya, na kuepa kusema uongo. Jiepushe na uovu, utende mema; utafute amani na kuizingatia. Mwenyezi-Mungu huwaangalia waadilifu, na kusikiliza malalamiko yao; lakini huwapinga watu watendao maovu, awafutilie mbali kutoka duniani. Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia, na kuwaokoa katika taabu zao zote. Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo; huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa. Mateso ya mwadilifu ni mengi, lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote. Huvilinda viungo vya mwili wake wote, hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa. Ubaya huwaletea waovu kifo; wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa. Mwenyezi-Mungu huokoa maisha ya watumishi wake, wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa. (Zaburi ya Daudi) Ee Mwenyezi-Mungu, uwapinge hao wanaonipinga; uwashambulie hao wanaonishambulia. Utwae ngao yako na kingio lako, uinuke uje ukanisaidie! Chukua mkuki na sime yako dhidi ya wanaonifuatia. Niambie mimi kwamba utaniokoa. Waone haya na kuaibika, hao wanaoyanyemelea maisha yangu! Warudishwe nyuma kwa aibu, hao wanaozua mabaya dhidi yangu. Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, wakikimbizwa na malaika wa Mwenyezi-Mungu! Njia yao iwe ya giza na utelezi, wakifukuzwa na malaika wa Mwenyezi-Mungu! Maana walinitegea mitego bila sababu; walinichimbia shimo bila kisa chochote. Maangamizi yawapate wao kwa ghafla, wanaswe katika mtego wao wenyewe, watumbukie humo na kuangamia! Hapo mimi nitafurahi kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu; nitashangilia kwa kuwa yeye ameniokoa. Nitamwambia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote: “Wewe ee Mwenyezi-Mungu, hakuna aliye kama wewe! Wewe wawaokoa wanyonge makuchani mwa wenye nguvu, maskini na fukara mikononi mwa wanyanganyi.” Mashahidi wakorofi wanajitokeza; wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa mema yangu kwa mabaya; nami binafsi nimebaki katika ukiwa. Lakini wao walipokuwa wagonjwa, mimi nilivaa magunia kuonesha huzuni; nilijitesa kwa kujinyima chakula. Nilisali nikiwa nimeinamisha kichwa, kana kwamba namlilia rafiki au ndugu yangu. Nilikwenda huko na huko kwa huzuni, kama mtu anayeomboleza kifo cha mama yake. Lakini mimi nilipoanguka walikusanyika kunisimanga. Walikusanyika pamoja dhidi yangu. Watu nisiowajua walinirarua bila kukoma, wala hakuna aliyewazuia. Watu ambao huwadhihaki vilema, walinisagia meno yao kwa chuki. Ee Mwenyezi-Mungu, utatazama tu mpaka lini? Uniokoe kutoka kwenye mashambulio yao; uyaokoe maisha yangu na simba hao. Hapo nitakushukuru kati ya kusanyiko kubwa la watu; nitakutukuza kati ya jumuiya kubwa ya watu. Usiwaache maadui hao wabaya wanisimange, hao wanichukiao bure wafurahie mateso yangu. Maneno wasemayo si ya amani, wanazua maneno ya hila dhidi ya wananchi watulivu. Wananishtaki kwa sauti: “Haya! Haya! Tumeona wenyewe uliyotenda!” Lakini wewe Mwenyezi-Mungu waona jambo hilo, usinyamaze, ee Mwenyezi-Mungu, usikae mbali nami. Uinuke, ee Mwenyezi-Mungu, ukanitetee; uje, ee Mungu wangu, uangalie kisa changu. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, unitetee, ufanye kulingana na uadilifu wako; usiwaache maadui zangu wanisimange. Usiwaache wajisemee: “Tumefanikiwa tulivyotaka!” Au waseme: “Tumemmaliza huyu!” Waache hao wanaofurahia maafa yangu, washindwe wote na kufedheheka. Hao wote wanaojiona wema kuliko mimi, waone haya na kuaibika. Lakini wanaotaka kuona kuwa sina hatia, wapaaze sauti kwa furaha waseme daima: “Mwenyezi-Mungu ni mkuu mno! Hupendezwa na fanaka ya mtumishi wake.” Hapo nami nitatangaza uadilifu wako; nitasema sifa zako mchana kutwa. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu) Dhambi huongea na mtu mwovu, ndani kabisa moyoni mwake; jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake. Mwovu hujipendelea mwenyewe, hufikiri uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa. Kila asemacho ni uovu na uongo; ameacha kutumia hekima na kutenda mema. Alalapo huwaza kutenda maovu, hujiweka katika njia isiyo njema, wala haachani na uovu. Fadhili zako ee Mwenyezi-Mungu zaenea hata mbinguni; uaminifu wako wafika mawinguni. Uadilifu wako ni kama milima mikubwa, hukumu zako ni kama vilindi vya bahari. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama Jinsi gani zilivyo bora fadhili zako! Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako. Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako; wawanywesha kutoka mto wa wema wako. Wewe ndiwe asili ya uhai; kwa mwanga wako twaona mwanga. Uendelee kuwafadhili wale wanaokutambua; uzidi kuwa mwema kwa wanyofu wa moyo. Usikubali wenye majivuno wanivamie, wala watu waovu wanikimbize. Kumbe watendao maovu wameanguka; wameangushwa chini, hawawezi kuinuka. (Zaburi ya Daudi) Usihangaike kwa sababu ya waovu; usiwaonee wivu watendao mabaya. Maana hao watatoweka mara kama nyasi; watanyauka kama mimea mibichi. Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kutenda mema, upate kuishi katika nchi na kuwa salama. Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu, naye atakujalia unayotamani moyoni. Mkabidhi Mwenyezi-Mungu maisha yako; mtumainie yeye naye atafanya kitu. Ataufanya wema wako ungae kama mwanga, na uadilifu wako kama jua la adhuhuri. Tulia mbele ya Mwenyezi-Mungu, mngojee kwa saburi; usihangaike juu ya wale wanaofanikiwa, watu wanaofaulu katika mipango yao mibaya. Epuka hasira wala usiwe na ghadhabu; usihangaike maana hiyo huzidisha ubaya. Watu watendao mabaya wataangamizwa, bali wanaomtumaini Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi. Bado kitambo kidogo, naye mwovu atatoweka; utamtafuta pale alipokuwa, wala hutamwona. Lakini wapole wataimiliki nchi, hao watafurahia wingi wa fanaka. Mwovu hula njama dhidi ya mwadilifu, na kumsagia meno kwa chuki. Lakini Mwenyezi-Mungu humcheka mwovu, kwani ajua mwisho wake u karibu. Waovu huchomoa panga na kuvuta pinde zao, wapate kuwaua maskini na fukara; wawachinje watu waishio kwa unyofu. Lakini panga zao zitawapenya wao wenyewe, na pinde zao zitavunjwavunjwa. Afadhali mali kidogo ya mtu mwadilifu kuliko utajiri wa watu waovu wengi. Maana nguvu za waovu zitavunjwa, lakini Mwenyezi-Mungu huwategemeza waadilifu. Mwenyezi-Mungu hutunza maisha ya watu waaminifu, na urithi wao utadumu milele. Hawataaibika zikifika nyakati mbaya; siku za njaa watakuwa na chakula tele. Lakini waovu wataangamia, maadui za Mwenyezi-Mungu watanyauka kama maua nyikani; naam, watatoweka kama moshi. Mtu mwovu hukopa bila kurudisha; lakini mwadilifu hutoa kwa ukarimu. Waliobarikiwa na Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi, lakini waliolaaniwa naye watafutiliwa mbali. Mwenyezi-Mungu huziongoza nyayo za mtu, humlinda yule ampendezaye. Ajapoanguka, haanguki akabaki chini, kwa sababu Mwenyezi-Mungu humtegemeza. Nilikuwa kijana na sasa ni mzee; kamwe sijaona mwadilifu ameachwa na Mungu, au watoto wake wakiombaomba chakula. Daima huwapa wengine kwa furaha na kukopesha, na watoto wake ni baraka. Achana na uovu, utende mema, nawe utaishi nchini daima; maana Mwenyezi-Mungu hupenda uadilifu, wala hawaachi waaminifu wake. Huwalinda hao milele; lakini wazawa wa waovu wataangamizwa. Waadilifu wataimiliki nchi, na wataishi humo milele. Mtu mwadilifu husema maneno ya hekima, kwa ulimi wake hunena yaliyo ya haki. Huizingatia moyoni mwake sheria ya Mungu wake; naye hatetereki katika mwenendo wake. Mtu mwovu humvizia mtu mwema na kujaribu kumuua; lakini Mwenyezi-Mungu hatamtia mtu mwema makuchani mwake, wala kumwacha apatilizwe akishtakiwa. Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kushika njia yake, naye atakukuza uimiliki nchi, na kuwaona waovu wakiangamizwa. Nilimwona mwovu mdhalimu sana, alijiweka juu ya wote kama mierezi ya Lebanoni! Baadaye nikapita hapo, naye hakuwapo tena; nikamtafuta, lakini hakuonekana tena. Mwangalie mtu mwema, mtu mwadilifu; mtu anayependa amani hujaliwa wazawa. Lakini wakosefu wote wataangamizwa; na wazawa wao watafutiliwa mbali. Mwenyezi-Mungu huwaokoa waadilifu, na kuwalinda wakati wa taabu. Mwenyezi-Mungu huwasaidia na kuwaokoa; huwatoa makuchani mwa waovu na kuwaokoa, maana wanakimbilia usalama kwake. (Zaburi ya Daudi ya matoleo) Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako; usiniadhibu kwa ghadhabu yako. Mishale yako imenichoma; mkono wako umenigandamiza. Hamna mahali nafuu mwilini mwangu, kwa sababu umenikasirikia; hamna penye afya hata mifupani mwangu, kwa sababu ya dhambi yangu. Nimefunikwa kabisa na dhambi zangu, zinanilemea kama mzigo mzito mno kwangu. Madonda yangu yameoza na kunuka, na hayo ni matokeo ya ujinga wangu. Nimepindika mpaka chini na kupondeka; mchana kutwa nazunguka nikiomboleza. Viungo vyangu vimeshambuliwa na homa; mwilini mwangu hamna nafuu yoyote. Nimelegea na kupondekapondeka; nasononeka kwa kusongwa moyoni. Ee Bwana, wewe wajua tazamio langu lote; kwako hakikufichika kilio changu. Moyo wanidunda, nguvu zimeniishia; hata macho yangu nayo yamekwisha fifia. Rafiki na wenzangu wanaepa kuona mateso yangu, na jamaa zangu wanakaa mbali nami. Wanaotaka kuniua wanatega mitego yao; wanaonitakia niumie wanatishia kuniangamiza. Mchana kutwa wanafanya mipango dhidi yangu. Lakini mimi nimekuwa kama kiziwi, sisikii; nimekuwa kama bubu asiyeweza kusema kitu. Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia, kama mtu asiye na chochote cha kujitetea. Lakini ninakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu; wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, ndiwe utakayenijibu. Nakuomba tu maadui wasinisimange, wasione fahari juu ya kuanguka kwangu. Karibu sana nitaanguka; nakabiliwa na maumivu ya daima. Naungama uovu wangu; dhambi zangu zanisikitisha. Maadui zangu hawajambo, wana nguvu; ni wengi mno hao wanaonichukia bure. Hao wanaonilipa maovu kwa wema wangu, wananipinga kwa sababu natenda mema. Usinitupe, ee Mwenyezi-Mungu; ee Mungu wangu, usikae mbali nami. Uje haraka kunisaidia; ewe Mwenyezi-Mungu, uliye wokovu wangu. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi) Nilisema: “Nitayachunga maisha yangu, nisije nikatenda dhambi kwa usemi wangu. Nitafunga mdomo wangu waovu wawapo karibu nami.” Nilikuwa kama bubu, bila kusema kitu, nilinyamaza lakini sikupata nafuu. Mateso yangu yalizidi kuwa makali, mahangaiko yangu yakaniunguza moyoni. Kadiri nilivyowaza ndivyo nilivyotaabika, kisha maneno haya yakanitoka: “Ee Mwenyezi-Mungu, unijulishe mwisho wangu, siku zangu za kuishi zimenibakia ngapi, nijue yapitavyo kasi maisha yangu!” Kumbe umenipimia maisha mafupi sana! Maisha yangu si kitu mbele yako. Hakika, kila binadamu ni kama pumzi tu! Kweli, kila mtu anapita kama kivuli; jitihada zake zote ni bure tu; anakusanya mali, asijue atakayeipata! Na sasa, ee Bwana, ninatazamia nini? Tumaini langu ni kwako wewe! Uniokoe katika makosa yangu yote; usikubali wapumbavu wanidhihaki. Niko kama bubu, sisemi kitu, kwani wewe ndiwe uliyetenda hayo. Usiniadhibu tena; namalizika kwa mapigo yako. Unapomwadhibu mtu dhambi zake kwa kumkemea, unaharibu kama nondo kile akipendacho. Hakika, kila binadamu ni kama pumzi tu! Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu; usikilize kilio changu, usikae kimya ninapolia. Maana, mimi ni kama mgeni tu apitaye, ni msafiri kama walivyokuwa wazee wangu wote. Uache kunitazama nipate kufurahi kidogo, kabla sijaaga dunia, na kutoweka kabisa. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Nilimngojea Mwenyezi-Mungu kwa uvumilivu, akanielekea na kukisikia kilio changu. Aliniondoa katika shimo la hatari, alinitoa katika matope ya dimbwi, akanisimamisha salama juu ya mwamba, na kuziimarisha hatua zangu. Alinifundisha wimbo mpya, wimbo wa sifa kwa Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, na kumtumainia Mwenyezi-Mungu. Heri mtu anayemtumainia Mwenyezi-Mungu; mtu asiyejiunga na watu wenye majivuno, watu waliopotoka kwa kuabudu miungu ya uongo. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umetufanyia mengi ya ajabu, na mipango yako juu yetu haihesabiki; hakuna yeyote aliye kama wewe. Kama ningeweza kusimulia hayo yote, idadi yake ingenishinda. Wewe hutaki tambiko wala sadaka, tambiko za kuteketeza wala za kuondoa dhambi; lakini umenipa masikio nikusikie. Ndipo niliposema: “Niko tayari; ninayotakiwa kufanya yameandikwa katika kitabu cha sheria; kutimiza matakwa yako, ee Mungu wangu ni furaha yangu, sheria yako naishika kwa moyo wangu wote!” Nimesimulia habari njema za ukombozi, mbele ya kusanyiko kubwa la watu. Kama ujuavyo ee Mwenyezi-Mungu, mimi sikujizuia kuitangaza. Sikuuficha moyoni mwangu ukombozi ulionijalia, nimetangaza daima kuwa wewe ni mwokozi mwaminifu; sikulificha kusanyiko kubwa la watu fadhili zako na uaminifu wako. Ee Mwenyezi-Mungu, usininyime huruma yako! Fadhili zako na uaminifu wako vinihifadhi daima. Maafa yasiyohesabika yanizunguka, maovu yangu yanikaba hata siwezi kuona; ni mengi kuliko nywele kichwani mwangu, nami nimevunjika moyo. Upende ee Mwenyezi-Mungu kuniokoa; ee Mwenyezi-Mungu, uje haraka kunisaidia. Wanaonuia kuniangamiza, na waaibike na kufedheheka! Hao wanaotamani niumie, na warudi nyuma na kuaibika! Hao wanaonisimanga, na wapumbazike kwa kushindwa kwao! Lakini wote wale wanaokutafuta wafurahi na kushangilia kwa sababu yako. Wapendao wokovu wako, waseme daima: “Mwenyezi-Mungu ni Mkuu!” Mimi ni maskini na fukara, ee Bwana; lakini ee Bwana wewe wanikumbuka. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu; uje, ee Mungu wangu, usikawie! (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Heri mtu anayewajali maskini; Mwenyezi-Mungu atamwokoa wakati wa shida. Mwenyezi-Mungu atamlinda na kumweka hai, naye atafanikiwa katika nchi; Mungu hatamwacha makuchani mwa maadui zake. Mwenyezi-Mungu atamsaidia awapo mgonjwa, atamponya maradhi yake yote. Nami nilisema: “Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu, unihurumie maana nimekukosea wewe.” Madui zangu husema vibaya juu yangu: “Atakufa lini na jina lake litoweke!” Wanitembeleapo husema maneno matupu; wanakusanya mabaya juu yangu, na wafikapo nje huwatangazia wengine. Wote wanichukiao hunongonezana juu yangu; wananiwazia mabaya ya kunidhuru. Husema: “Maradhi haya yatamuua; hatatoka tena kitandani mwake!” Hata rafiki yangu wa moyoni niliyemwamini, rafiki ambaye alishiriki chakula changu, amegeuka kunishambulia! Ee Mwenyezi-Mungu, unionee huruma! Unipe nafuu, nami nitawalipiza. Hivyo nitajua kwamba unapendezwa nami, maadui zangu wasipopata fahari juu yangu. Wewe umenitegemeza kwani natenda mema; waniweka mbele yako milele. Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele! Amina! Amina! (Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Wakorahi) Kama paa atamanivyo maji ya kijito, ndivyo ninavyokutamani, ee Mungu wangu! Naona kiu ya Mungu, kiu ya Mungu aliye hai. Nitafika lini kwake na kuuona uso wake? Machozi yamekuwa chakula changu mchana na usiku, waliponiambia kila siku: “Yuko wapi Mungu Wako!” Nakumbuka tena mambo haya kwa majonzi moyoni mwangu: Jinsi nilivyokwenda na umati wa watu, nikawaongoza kwenda nyumbani kwa Mungu wakipiga vigelegele vya shukrani; umati wa watu wakifanya sherehe! Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo ndani mwangu? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena yeye aliye msaada wangu na Mungu wangu. Nimesongwa na huzuni moyoni mwangu, kwa hiyo ninakukumbuka wewe, ee Mungu, kutoka katika eneo la Yordani, kutoka mlima Hermoni na Mizari. Nimeporomoshewa mafuriko ya maji mafuriko ya maji yaja karibu nayo yaita maporomoko mapya. Mawimbi na mapigo yako yamenikumba. Mwenyezi-Mungu atanijalia fadhili zake mchana; nami nimwimbie wimbo wa sifa usiku, nimwombe Mungu anipaye uhai. Namwambia Mungu, mwamba wangu: “Kwa nini umenisahau? Yanini niende huko na huko nikiomboleza kwa kudhulumiwa na adui yangu?” Nimepondwa kwa matukano yao, wanaponiuliza kila siku: “Yuko wapi, Mungu wako!” Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena Mungu, aliye msaada wangu na Mungu wangu. (Zaburi ya 42 yaendelea) Onesha kuwa sina hatia ee Mungu; utetee kisa changu dhidi ya watu wabaya; uniokoe na watu waongo na waovu. Nakimbilia usalama kwako ee Mungu; kwa nini umenitupilia mbali? Yanini niende huko na huko nikiomboleza kwa kudhulumiwa na adui yangu? Upeleke mwanga na ukweli wako viniongoze, vinipeleke kwenye mlima wako mtakatifu, kwenye makao yako. Hapo, ee Mungu, nitakwenda madhabahuni pako; nitakuja kwako, ee Mungu, furaha yangu kuu. Nitakusifu kwa zeze, ee Mungu, Mungu wangu. Mbona ninahuzunika hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo ndani mwangu? Nitamtumainia Mungu, nitamsifu tena yeye aliye msaada wangu na Mungu wangu. (Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Wakorahi) Ee Mungu, sisi tumesikia kwa masikio yetu, wazee wetu wametusimulia mambo uliyotenda nyakati zao, naam, mambo uliyotenda hapo kale: Kwa mkono wako mwenyewe uliyafukuza mataifa mengine, na mahali pao ukawakalisha watu wako; uliyaadhibu mataifa mengine, na kuwafanikisha watu wako. Watu wako hawakuitwaa nchi kwa silaha zao, wala hawakupata ushindi kwa nguvu zao; ila uliwasalimisha kwa mkono wako mwenyewe, kwa kuwaangazia uso wako, kwani wewe uliwapenda. Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu! Wawajalia ushindi wazawa wa Yakobo. Kwa nguvu yako twawashinda maadui zetu, kwa jina lako twawakanyaga wanaotushambulia. Mimi siutegemei upinde wangu, wala upanga wangu hauwezi kuniokoa. Wewe ndiwe uliyetuokoa na maadui zetu; uliwavuruga wale waliotuchukia. Daima tutaona fahari juu yako, ee Mungu; tutakutolea shukrani milele. Lakini sasa umetuacha na kutufedhehesha; huandamani tena na majeshi yetu. Umetufanya tuwakimbie maadui zetu, nao wakaziteka nyara mali zetu. Umetufanya kama kondoo wanaopelekwa kuchinjwa; umetutawanya kati ya mataifa mengine. Umewauza watu wako kwa bei ya chini; wala hukupata faida yoyote. Umetufanya kuwa kioja kwa jirani zetu, nao wanatudhihaki na kutucheka. Umetufanya tudharauliwe na watu wa mataifa; wanatutikisia vichwa vyao kwa kutupuuza. Mchana kutwa fedheha yaniandama, na uso wangu umejaa aibu tele kwa maneno na madharau ya wenye kunitukana, kwa kukabiliwa na maadui zangu na walipiza kisasi. Hayo yote yametupata sisi ijapokuwa hatujakusahau, wala hatujavunja agano lako. Hatujakuasi wewe, wala hatujaziacha njia zako. Hata hivyo umetuacha hoi kati ya wanyama wakali; umetuacha katika giza kuu. Tungalikuwa tumekusahau wewe Mungu wetu, tukamkimbilia mungu wa uongo, ee Mungu, ungalikwisha jua jambo hilo, kwa maana wewe wazijua siri za moyoni. Lakini kwa ajili yako twakikabili kifo kila siku; tunatendewa kama kondoo wanaopelekwa kuchinjwa. Amka, ee Bwana! Mbona umelala? Inuka! Tafadhali usitutupe milele! Mbona wajificha mbali nasi, na kusahau dhiki na mateso yetu? Tumedidimia hata mavumbini, tumegandamana na ardhi. Uinuke, uje kutusaidia! Utukomboe kwa sababu ya fadhili zako. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Utenzi wa Wakorahi; utenzi wa mapenzi) Moyo wangu umejaa mawazo mema: Namtungia mfalme shairi langu, ulimi wangu ni kama kalamu ya mwandishi stadi. Wewe u mzuri kuliko wanadamu wote, maneno yako ni fadhili tupu. Kwa hiyo Mungu amekubariki milele. Jifunge upanga wako, ewe shujaa! Wewe ni mtukufu na mwenye fahari. Songa mbele kwa utukufu upate ushindi, utetee ukweli na kulinda haki. Mkono wako utende mambo makuu. Mishale yako ni mikali, hupenya mioyo ya maadui za mfalme; nayo mataifa huanguka chini yako. Kiti chako cha enzi ni imara, chadumu milele kama cha Mungu. Wewe watawala watu wako kwa haki. Wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuteua, na kukupa furaha kuliko wenzako. Mavazi yako yanukia marashi na udi, wanamuziki wakuimbia katika majumba ya pembe za ndovu. Binti za wafalme ni baadhi ya wanaokulaki, naye malkia amesimama kulia kwako, amevaa mapambo ya dhahabu safi ya Ofiri. Sikiliza binti, ufikirie! Tega sikio lako: Sahau sasa watu wako na jamaa zako. Uzuri wako wamvutia mfalme; yeye ni bwana wako, lazima umtii. Watu wa Tiro watakuletea zawadi; matajiri watataka upendeleo wako. Binti mfalme anaingia mzuri kabisa! Vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu. Akiwa amevalia vazi la rangi nyingi, anaongozwa kwa mfalme, akisindikizwa na wasichana wenzake; nao pia wanapelekwa kwa mfalme. Kwa furaha na shangwe wanafika huko, na kuingia katika jumba la mfalme. Ee mfalme, utapata watoto wengi watakaotawala mahali pa wazee wako; utawafanya watawale duniani kote. Nitalifanya jina lako litukuzwe katika vizazi vyote, nayo mataifa yatakusifu daima na milele. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi. Mtindo wa Alamothi) Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu; yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu. Kwa hiyo hatutaogopa chochote, dunia ijapoyeyuka na milima kutikisika kutoka baharini; hata kama bahari ikichafuka na kutisha, na milima ikatetemeka kwa machafuko yake. Kuna mto ambao maji yake hufurahisha mji wa Mungu, makao matakatifu ya Mungu Mkuu. Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa; Mungu ataupa msaada alfajiri na mapema. Mataifa yaghadhibika na tawala zatikisika; Mungu anguruma nayo dunia yayeyuka. Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu. Njoni mwone matendo ya Mwenyezi-Mungu; oneni maajabu aliyoyafanya duniani. Hukomesha vita popote duniani, huvunjavunja pinde na mikuki, nazo ngao huziteketeza. Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi) Enyi watu wote, pigeni makofi! Msifuni Mungu kwa sauti za shangwe! Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu, anatisha. Yeye ni Mfalme mkuu wa ulimwengu wote. Ametuwezesha kuwashinda watu wa mataifa, ameyaweka mataifa chini ya mamlaka yetu. Ametuchagulia nchi hii iwe urithi wetu, ambayo ni fahari ya Yakobo anayempenda. Mungu amepanda juu na vigelegele, Mwenyezi-Mungu na sauti ya tarumbeta. Mwimbieni Mungu sifa, mwimbieni! Mwimbieni mfalme wetu sifa, mwimbieni! Mwimbieni Mungu sifa kwa tenzi; maana yeye ni mfalme wa ulimwengu wote. Mungu anayatawala mataifa yote; amekaa katika kiti chake cha enzi kitakatifu. Viongozi wa watu wa mataifa wanakusanyika, wanajiunga na watu wa Mungu wa Abrahamu, maana nguvu zote duniani ni zake Mungu, yeye ametukuka sana. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi) Mwenyezi-Mungu, ni mkuu; astahili kusifiwa sana katika mji wake na mlima wake mtakatifu. Mlima Siyoni huko kaskazini, wapendeza kwa urefu; mji wa Mfalme mkuu ni furaha ya ulimwengu. Mungu anazilinda ngome zake; yeye amejionesha kuwa ngome ya usalama. Wafalme walikusanyika, wakaenda pamoja kushambulia. Lakini walipouona mji wa Siyoni, wakashangaa; wakashikwa na hofu, wakatimua mbio. Hofu kuu iliwashika, wakasikia uchungu kama mama anayejifungua, kama waliokumbwa na kimbunga cha mashariki ambacho huzivunjavunja meli za Tarshishi. Yote tuliyosikia tumejionea wenyewe katika mji wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, naam, katika mji wa Mungu wetu; Mungu atauimarisha milele. Ee Mungu, twazitafakari fadhili zako, tukiwa hekaluni mwako. Jina lako lasifika kila mahali, sifa zako zaenea popote duniani. Kwa mkono wako umetenda kwa haki; watu wa Siyoni na wafurahi! Watu wa Yuda na washangilie, kwa sababu ya maamuzi yako ya haki! Tembeeni huko Siyoni mkauzunguke, mkaihesabu minara yake. Zitazameni kuta zake na kuchunguza ngome zake; mpate kuvisimulia vizazi vijavyo, kwamba: “Huyu ni Mungu, Mungu wetu milele! Atakuwa kiongozi wetu milele!” (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi) Sikieni jambo hili enyi watu wote! Tegeni sikio enyi wakazi wote wa dunia; sikilizeni nyote, wakubwa kwa wadogo, matajiri na maskini kwa pamoja. Maneno yangu yatakuwa mazitomazito; mimi nitasema maneno ya hekima. Nitatega sikio nisikilize methali, nitafafanua kitendawili kwa muziki wa zeze. Ya nini niogope siku mbaya, wakati nizungukwapo na uovu wa adui? Watu waovu hutegemea mali zao, hujisifia wingi wa utajiri wao. Lakini binadamu hawezi kamwe kujikomboa mwenyewe; hawezi kumlipa Mungu bei ya maisha yake, maana fidia ya maisha ni kubwa mno. Hawezi kutoa kitu chochote kinachotosha, kimwezeshe aendelee kuishi daima, asipate kuonja kaburi. Yeye afahamu kuwa hata wenye hekima hufa, wapumbavu hali kadhalika na watu wajinga. Wote hao huwaachia wengine mali zao. Makaburi ni makao yao hata milele; ni makao yao vizazi hata vizazi, ingawa hapo awali walimiliki ardhi. Binadamu hatadumu katika fahari yake; atakufa tu kama mnyama. Hayo ndiyo yawapatao wanaojiamini kipumbavu, ndio mwisho wa wale wanaojivunia mali zao. Wataongozwa kama kondoo hadi kuzimu, kifo kitakuwa mchungaji wao. Watashuka moja kwa moja kaburini. Miili yao itaozea huko, Kuzimu kutakuwa makao yao. Lakini Mungu ataniokoa na kuzimu. Atanisalimisha kutoka huko. Usihangaike ukiona mtu anatajirika, wala mali yake ikiongezeka zaidi na zaidi. Maana atakapokufa hatachukua chochote, mali yake haitashuka huko chini pamoja naye. Ajapojikuza katika maisha haya, na kusifiwa kwa sababu ya kufanikiwa, atajiunga na wazee waliomtangulia kufa, ambao hawawezi kuona tena mwanga. Binadamu hatadumu milele katika fahari yake, atakufa tu kama mnyama. (Zaburi ya Asafu) Mungu wa nguvu Mwenyezi-Mungu, amenena, amewaita wakazi wa dunia, tokea mawio ya jua hadi machweo yake. Kutoka Siyoni, mji mzuri mno, Mungu anajitokeza, akiangaza. Mungu wetu anakuja, na sio kimyakimya: Moto uunguzao wamtangulia, na dhoruba kali yamzunguka. Kutoka juu anaziita mbingu na dunia; zishuhudie akiwahukumu watu wake: “Nikusanyieni waaminifu wangu, waliofanya agano nami kwa tambiko!” Mbingu zatangaza uadilifu wa Mungu; kwamba Mungu mwenyewe ni hakimu. “Sikilizeni watu wangu, ninachosema! Israeli, natoa ushahidi dhidi yako. Mimi ni Mungu! Mimi ni Mungu wako! Sikukaripii kwa sababu ya tambiko zako; hujaacha kunitolea tambiko za kuteketeza. Kwa kweli sina haja na fahali wa zizi lako, wala beberu wa mifugo yako; maana wanyama wote porini ni mali yangu, na maelfu ya wanyama milimani ni wangu. Ndege wote wa mwitu ni mali yangu, na viumbe vyote hai mashambani ni vyangu. Kama ningeona njaa singekuambia wewe, maana ulimwengu na vyote vilivyomo ni vyangu. Je, wadhani nala nyama ya fahali, au Kunywa damu ya mbuzi? Shukrani iwe ndio tambiko yako kwa Mungu mtimizie Mungu Aliye Juu ahadi zako. Uniite wakati wa taabu, nami nitakuokoa, nawe utaniheshimu.” Lakini Mungu amwambia mtu mwovu: “Ya nini kuzitajataja tu sheria zangu? Kwa nini unasemasema juu ya agano langu? Wewe wachukia kuwa na nidhamu, na maneno yangu hupendi kuyafuata. Ukimwona mwizi unaandamana naye, na wazinzi unashirikiana nao. Uko tayari daima kunena mabaya; kazi ya ulimi wako ni kutunga uongo. Wakaa kitako kumsengenya binadamu mwenzako, naam, kumchongea ndugu yako mwenyewe. Umefanya hayo yote nami nimenyamaa. Je, wadhani kweli mimi ni kama wewe? Lakini sasa ninakukaripia, ninakugombeza waziwazi. “Fikirini vizuri jambo hili, enyi msionijali, la sivyo nitawaangamizeni, wala hapatakuwa na wa kuwaokoeni. Anayenipa shukrani kama tambiko yake, huyo ndiye anayeniheshimu; yeyote anayedumu katika njia yangu, huyo ndiye nitakayemwokoa.” (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kosa lake na Bathsheba) Nihurumie, Ee Mungu, kadiri ya fadhili zako; ufutilie mbali makosa yangu, kadiri ya wingi wa huruma yako. Unioshe kabisa hatia yangu; unisafishe dhambi yangu. Nakiri kabisa makosa yangu, daima naiona waziwazi dhambi yangu. Nimekukosea wewe peke yako, nimetenda yaliyo mabaya mbele yako. Uamuzi wako ni wa haki hukumu yako haina lawama. Mimi ni mkosefu tangu kuzaliwa kwangu, mwenye dhambi tangu tumboni mwa mama yangu. Wewe wataka unyofu wa ndani; hivyo nifundishe hekima moyoni. Unitakase kwa husopo, nitakate; unioshe niwe mweupe pe. Nijaze furaha na shangwe, nifurahishe tena, mimi ambaye uliniponda. Ugeuke, usiziangalie dhambi zangu; uzifute hatia zangu zote. Uniumbie moyo safi, ee Mungu, uweke ndani yangu roho mpya na thabiti. Usinitupe mbali nawe; usiniondolee roho yako takatifu. Unifanye nifurahi tena kwa kuniokoa, utegemeze ndani yangu moyo wa utii. Hapo nitawafunza wakosefu njia yako, nao wenye dhambi watarudi kwako. Uniokoe na hatia ya umwagaji damu, ee Mungu, Mungu mwokozi wangu, nami nitaimba kwa sauti kuwa umeniokoa. Uniwezeshe kusema, ee Bwana, midomo yangu itangaze sifa zako. Kwa kweli wewe hupendezwi na tambiko, ama sivyo mimi ningalikutolea. Wewe huna haja na tambiko za kuteketezwa. tambiko yangu kwako ee Mungu, ni moyo mnyofu; wewe, ee Mungu, hukatai moyo mnyofu na mtiifu. Ee Mungu, upende kuutendea mema mji wa Siyoni; uzijenge tena upya kuta za mji wa Yerusalemu. Hapo utapendezwa na tambiko za kweli: Sadaka za kuteketezwa na za kuteketezwa nzima; mafahali watatolewa tambiko madhabahuni pako. (Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Daudi baada ya Doegi, Mwedomu, kumwendea Shauli na kumjulisha kuwa Daudi amekwenda nyumbani kwa Abimeleki) Mbona, ewe jitu, wajivunia ubaya wako dhidi ya wenye kumcha Mungu? Kila wakati unawaza maangamizi; ulimi wako ni kama wembe mkali! Unafikiria tu kutenda mabaya. Wewe wapenda uovu kuliko wema, wapenda uongo kuliko ukweli. Ewe mdanganyifu mkuu, wapenda mambo ya kuangamiza wengine. Kwa hivyo Mungu atakuangamiza milele, atakunyakua na kukuondoa nyumbani mwako; atakungoa katika nchi ya walio hai. Waadilifu wataona hayo na kuogopa, kisha watakucheka na kusema: “Tazameni yaliyompata mtu huyu! Yeye hakutaka Mungu awe kimbilio lake; bali alitegemea wingi wa mali yake, na kutafuta humo usalama wake!” Lakini mimi ni kama mzeituni mbichi, unaostawi katika nyumba ya Mungu. Nazitegemea fadhili zake milele na milele. Ee Mungu, nitakushukuru daima, kwa ajili ya mambo uliyofanya. Nitatangaza kwamba wewe ni mwema, mbele ya watu wako waaminifu. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Mahalathi. Utenzi wa Daudi) Wapumbavu hujisemea moyoni: “Hakuna Mungu!” Wote wamepotoka kabisa, wametenda mambo ya kuchukiza; hakuna hata mmoja atendaye jema. Mungu anawaangalia wanadamu kutoka mbinguni, aone kama kuna yeyote mwenye busara, kama kuna yeyote anayemtafuta Mungu. Lakini wote wamekosa, wote wamepotoka pamoja, hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja. “Je, hao watendao maovu hawana akili? Wanawatafuna watu wangu kama mikate; wala hawanijali mimi Mungu!” Hapo watashikwa na hofu kubwa, hofu ambayo hawajapata kuiona; maana Mungu ataitawanya mifupa ya adui, hao wataaibika maana Mungu amewakataa. Laiti ukombozi wa Israeli ungefika kutoka Siyoni! Mungu atakaporekebisha hali ya watu wake, wazawa wa Yakobo watashangilia; Waisraeli watafurahi. (Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Utenzi wa Daudi wakati mtu mmoja kutoka Zifu alipomwendea Shauli na kumjulisha kuwa Daudi amejificha kwao.) Uniokoe, ee Mungu, kwa jina lako; unitetee kwa nguvu yako. Uisikie, ee Mungu, sala yangu; uyategee sikio maneno ya kinywa changu. Watu wenye kiburi wananishambulia; wakatili wanayawinda maisha yangu, watu ambao hawamjali Mungu. Najua Mungu ni msaada wangu, Mwenyezi-Mungu hutegemeza maisha yangu. Yeye atawaadhibu maadui zangu kwa uovu wao wenyewe; kwa uaminifu wako, ee Mungu, uwaangamize. Nitakutolea tambiko kwa moyo mkunjufu; nitakushukuru kwa kuwa ni vema. Maana umeniokoa katika taabu zangu zote, nami nimewaona maadui zangu wameshindwa. (Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Utenzi wa Daudi) Ee Mungu, tega sikio usikie sala yangu; usiangalie pembeni ninapokuomba. Unisikilize na kunijibu; nimechoshwa na lalamiko langu. Nina hofu kwa vitisho vya maadui zangu, na kwa kudhulumiwa na watu waovu. Watu waovu wananitaabisha, kwa hasira wananifanyia uhasama. Moyo wangu umejaa hofu, vitisho vya kifo vimenisonga. Natetemeka kwa hofu kubwa, nimevamiwa na vitisho vikubwa. Laiti ningekuwa na mabawa kama njiwa! Ningeruka mbali na kupata pumziko; naam, ningesafiri mbali sana, na kupata makao jangwani. Ningekimbilia mahali pa usalama, mbali na upepo mkali na dhoruba. Ee Bwana, uwaangamize na kuvuruga lugha yao; maana naona ukatili na ugomvi mjini, vikiuzunguka usiku na mchana, na kuujaza maafa na jinai. Uharibifu umeenea pote mjini, uhasama na udhalimu kila mahali. Kama adui yangu angenitukana, ningeweza kustahimili hayo; kama mpinzani wangu angenidharau, ningeweza kujificha mbali naye. Kumbe, lakini, ni wewe mwenzangu; ni wewe rafiki yangu na msiri wangu! Sisi tulizoea kuzungumza kirafiki; pamoja tulikwenda nyumbani kwa Mungu. Acha kifo kiwafumanie maadui zangu; washuke chini Kuzimu wangali hai; maana uovu umewajaa moyoni mwao. Lakini mimi namlilia Mungu, naye Mwenyezi-Mungu ataniokoa. Jioni, asubuhi na adhuhuri, nalalama na kulia, naye ataisikia sauti yangu. Atanikomboa salama katika vita ninayoikabili, kwa maana maadui zangu ni wengi. Mungu atawalaye tangu milele, atanisikia na kuwaaibisha maadui zangu, maana hawapendi kujirekebisha, wala hawamwogopi Mungu. Mwenzangu amewashambulia rafiki yake, amevunja mapatano yake. Maneno yake ni laini kuliko siagi, lakini mawazo yake ni ya kufanya vita. Maneno yake ni mororo kama mafuta, lakini yanakata kama upanga mkali. Mwachie Mwenyezi-Mungu mzigo wako, naye atakutegemeza; kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe. Wewe, ee Mungu, utawaporomosha shimoni chini kabisa, watu hao wauaji na wadanganyifu; hao hawatafikia nusu ya maisha yao. Lakini mimi nitakutumainia wewe ee Mungu! (Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Njiwa Mkimya wa Mbali”. Utenzi wa Daudi baada ya kukamatwa na Wafilisti kule Gathi) Ee Mungu, unionee huruma, maana watu wananishambulia. Mchana kutwa maadui wananidhulumu. Mchana kutwa maadui zangu wananishambulia; ni wengi mno hao wanaonipiga vita. Ee Mungu Mkuu, hofu inaponishika, mimi nakutumainia wewe. Namtumainia Mungu na kusifu neno lake; namtumainia Mungu, wala siogopi. Binadamu dhaifu atanifanya nini? Mchana kutwa wanapotosha kisa changu; mawazo yao yote ni ya kunidhuru. Wanakutana kupanga na kunivizia; wanachunguza yote nifanyayo; wananiotea kwa shabaha ya kuniua. Ee Mungu, uwalipe kwa kadiri ya uovu wao, uwaangushe hao waovu kwa hasira yako. Wewe wakujua kusukwasukwa kwangu; waweka kumbukumbu ya machozi yangu yote. Je, yote si yamo kitabuni mwako? Kila mara ninapokuomba msaada wako, maadui zangu wanarudishwa nyuma. Najua kweli Mungu yuko upande wangu. Namtumaini Mungu na kusifu neno lake; namtumainia Mwenyezi-Mungu na kusifu neno lake. Namtumainia Mungu, wala siogopi. Binadamu atanifanya nini? Ee Mungu, nitatimiza ahadi zangu kwako; nitakutolea tambiko za shukrani, Maana umeniokoa katika kifo, naam, umenilinda nisianguke chini; nipate kuishi mbele yako, ee Mungu, katika mwanga wa uhai. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi alipomponyoka Shauli na kujificha pangoni) Unihurumie, ee Mungu, unihurumie, maana kwako nakimbilia usalama. Kivulini mwa mabawa yako nitakimbilia usalama, hata hapo dhoruba ya maangamizi itakapopita. Namlilia Mungu Mkuu, Mungu anikamilishiaye nia yake. Atanipelekea msaada toka mbinguni na kuniokoa; atawaaibisha hao wanaonishambulia. Mungu atanionesha fadhili zake na uaminifu wake! Mimi nimezungukwa na maadui, wenye uchu wa damu kama simba; meno yao ni kama mikuki na mishale, ndimi zao ni kama panga kali. Utukuzwe, ee Mungu, juu ya mbingu! Utukufu wako uenee duniani kote! Maadui wamenitegea wavu waninase, nami nasononeka kwa huzuni. Wamenichimbia shimo njiani mwangu, lakini wao wenyewe wametumbukia humo. Niko thabiti moyoni, ee Mungu, naam, niko thabiti moyoni; nitaimba na kukushangilia! Amka, ee nafsi yangu! Amkeni, enyi kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko! Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa; nitakuimbia sifa kati ya mataifa. Fadhili zako zaenea hata juu ya mbingu, uaminifu wako wafika hata mawinguni. Utukuzwe, ee Mungu, juu ya mbingu! Utukufu wako uenee duniani kote! (Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi) Enyi watawala, je, mwahukumu kwa haki kweli? Je, mnawahukumu watu kwa adili? La! Nyinyi mwafikiria tu kutenda maovu; nyinyi wenyewe mwaeneza dhuluma nchini. Waovu wamepotoka tangu kuzaliwa kwao, waongo hao, wamekosa tangu walipozaliwa. Wana sumu kama sumu ya nyoka; viziwi kama joka lizibalo masikio, ambalo halisikii hata sauti ya mlozi, au utenzi wa mganga stadi wa uchawi. Ee Mungu, wavunje meno yao, yangoe, ee Mwenyezi-Mungu, meno ya simba hao. Watoweke kama maji yanayodidimia mchangani, kama nyasi wakanyagwe na kunyauka, watoweke kama konokono ayeyukavyo, kama mimba iliyoharibika isiyoona kamwe jua! Kabla hawajatambua, wangolewe kama miiba, michongoma au magugu. Kwa hasira ya Mungu, wapeperushwe mbali, wakiwa bado hai. Waadilifu watafurahi waonapo waovu wanaadhibiwa; watatembea katika damu ya watu wabaya. Watu wote watasema: “Naam, waadilifu hupata tuzo! Hakika yuko Mungu anayeihukumu dunia!” (Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi wakati Shauli alipotuma wapelelezi wamuue) Ee Mungu wangu, uniokoe na maadui zangu; unikinge na hao wanaonishambulia. Uniokoe na hao wanaotenda maovu; unisalimishe kutoka kwa hao wauaji! Tazama! Wananivizia waniue; watu wakatili wanachochea ugomvi dhidi yangu. Bila ya kosa, hatia au dhambi yangu, wanakimbia, ee Mwenyezi-Mungu, kujiweka tayari. Uinuke, ee Mwenyezi-Mungu, ukatazame na kunisaidia! Uinuke, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu Mwenye Nguvu, Mungu wa Israeli. Uamke, uwaadhibu hao watu wasiokujua; usiwaache hao wanaopanga ubaya. Kila jioni maadui hao hurudi wakibweka kama mbwa, na kuzungukazunguka mjini. Tazama, ni matusi tu yatokayo mdomoni mwao, maneno yao yanakata kama upanga mkali; tena wanafikiri hakuna anayewasikia. Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wawacheka; unawapuuza hao watu wote wasiokujua. Nitakungoja, ewe uliye nguvu yangu; maana wewe, ee Mungu, u ngome yangu. Mungu wangu utanijia na fadhili zako, utaniwezesha kuwaona maadui zangu wameshindwa. Usiwaue mara moja, watu wangu wasije wakasahau; ila uwayumbishe kwa nguvu yako, uwaporomoshe chini. Ee Bwana, wewe ndiwe ngao yetu! Wao hutenda dhambi kwa yote wasemayo, kwa hiyo na wanaswe katika kiburi chao! Kwa sababu ya laana na uongo wao, uwateketeze kwa hasira yako, uwateketeze wasiwepo tena; ili watu wote wajue kuwa wewe ee Mungu watawala wazawa wa Yakobo hata mpaka miisho ya dunia. Kila jioni maadui hao hurudi wakibweka kama mbwa, na kuzungukazunguka mjini. Hupitapita huko na huko wakitafuta mlo, na wasipotoshelezwa hunguruma. Lakini mimi nitaimba sifa za nguvu yako; nitashangilia asubuhi juu ya fadhili zako; maana wewe umekuwa ngome yangu na kimbilio langu wakati wa taabu. Ewe uliye nguvu yangu, nitakuimbia sifa; ee Mungu, wewe u ngome yangu; Mungu mwenye kunifadhili! (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Shushani Edut. Utenzi wa Daudi wa kufundisha, wakati alipopigana na Waaramu kutoka Naharaimu na Zoba, Yoabu aliporudi nyuma na kuwaua Waedomu 12,000 katika Bonde la Chumvi) Ee Mungu, umetutupa na kutuponda, umewaka hasira, tafadhali uturudishie nguvu. Umeitetemesha nchi na kuipasua; uzibe nyufa zake kwani inabomoka. Umewatwika watu wako mateso; tunayumbayumba kama waliolewa divai. Uwape ishara wale wanaokuheshimu, wapate kuuepa mshale. Uwasalimishe hao watu uwapendao; utuokoe kwa mkono wako, na kutusikiliza. Mungu amesema kutoka patakatifu pake “Sasa nitaigawa Shekemu kwa shangwe, Bonde la Sukothi nitalipima sehemusehemu. Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu; Efraimu ni kofia yangu ya chuma, na Yuda ni fimbo yangu ya enzi. Moabu ni kama bakuli langu la kunawia, kiatu changu nitaitupia Edomu kuimiliki. Nitapiga kelele ya ushindi juu ya Filistia.” Ni nani atakayenipeleka kwenye mji wa ngome? Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu? Je, umetuacha kabisa, ee Mungu? Wewe huendi tena na majeshi yetu! Utupatie msaada dhidi ya maadui zetu, maana msaada wa binadamu haufai kitu. Mungu akiwa upande wetu tutashinda, yeye atawaponda maadui zetu. (Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi) Ee Mungu, usikie kilio changu, usikilize sala yangu. Ninakulilia kutoka miisho ya dunia, nikiwa nimevunjika moyo. Uniongoze juu kwenye mwamba mkubwa maana wewe ndiwe kimbilio langu, kinga yangu imara dhidi ya adui. Naomba nikae nyumbani mwako milele nipate usalama chini ya mabawa yako. Ee Mungu, umezisikia ahadi zangu, umenijalia sehemu yangu unayowapa wale wakuchao. Umjalie mfalme maisha marefu, miaka yake iwe ya vizazi vingi. Atawale milele mbele yako, ee Mungu; fadhili na uaminifu wako vimlinde. Hivyo nitakuimbia nyimbo za sifa, nikizitekeleza ahadi zangu kila siku. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi) Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu, kwake watoka wokovu wangu. Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika. Hata lini mtanishambulia mimi? Hata lini nyinyi nyote mtanipiga, mimi niliye kama kiambaza kilichoinama, kama ukuta unaoanza kubomoka? Mmepanga kuniangusha toka mahali pangu pa heshima; furaha yenu ni kusema uongo. Kwa maneno, mnabariki, lakini moyoni mnalaani. Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu; kwake naliweka tumaini langu. Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika. Wokovu na fahari yangu vyatoka kwa Mungu; mwamba wangu mkuu na kimbilio langu ni Mungu. Enyi watu, mtumainieni Mungu daima; mfungulieni Bwana yaliyo moyoni mwenu. Mungu ndiye kimbilio la usalama wetu. Binadamu wote ni kama pumzi tu; wote, wakubwa kwa wadogo, hawafai kitu. Tena ukiwapima uzito hawafikii kilo, wote pamoja ni wepesi kuliko pumzi. Msitegemee dhuluma, msijisifie mali ya wizi; kama mali zikiongezeka, msizitegemee. Mungu ametamka mara moja, nami nimesikia tena na tena: Kwamba enzi ni mali yake Mungu; naam, nazo fadhili ni zake Bwana; humlipa kila mtu kadiri ya matendo yake. (Zaburi ya Daudi wakati alipokuwa katika jangwa la Yudea) Ee Mungu, wewe u Mungu wangu, nami nakutafuta kwa moyo; roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu; nina kiu kama nchi kavu isiyo na maji. Nimetaka kukuona patakatifuni pako, niione nguvu yako na utukufu wako. Fadhili zako ni bora kuliko maisha, nami nitakusifu kwa mdomo wangu. Nitakushukuru maisha yangu yote; nitainua mikono yangu na kukuomba. Roho yangu inafurahi kama kwa karamu na vinono; kwa shangwe nitaimba sifa zako. Niwapo kitandani ninakukumbuka, usiku kucha ninakufikiria; maana wewe umenisaidia daima. Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia. Roho yangu inaambatana nawe kabisa, mkono wako wa kulia wanitegemeza. Lakini hao wanaotaka kuyaangamiza maisha yangu, watatumbukia chini kwenye makao ya wafu. Watauawa kwa upanga, watakuwa chakula cha mbweha. Lakini mfalme atafurahi kwa sababu ya Mungu; wanaoahidi kwa jina la Mungu watamsifu, lakini vinywa vya waongo vitafumbwa. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Usikie, ee Mungu, lalamiko langu; yalinde maisha yangu na vitisho vya maadui. Unikinge na njama za waovu, na ghasia za watu wabaya. Wananoa ndimi zao kama upanga, wanafyatua maneno ya ukatili kama mishale. Toka mafichoni wamshambulia mtu mnyofu, wanamshambulia ghafla bila kuogopa. Wanashirikiana katika nia yao mbaya; wanapatana mahali pa kuficha mitego yao. Wanafikiri: “Hakuna atakayeweza kuiona.” Hufanya njama zao na kusema: “Sasa tumekamilisha mpango! Nani atagundua hila zetu?” Mipango ya siri imefichika moyoni mwa mtu! Lakini Mungu atawapiga mishale, na kuwajeruhi ghafla. Atawaangamiza kwa sababu ya maneno yao; kila atakayewaona atatikisa kichwa. Hapo watu wote wataogopa; watatangaza aliyotenda Mungu, na kufikiri juu ya matendo yake. Waadilifu watafurahi kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, na kukimbilia usalama kwake; watu wote wanyofu wataona fahari. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi: Wimbo) Wastahili sifa, ee Mungu, huko Siyoni, watu watakutimizia wewe ahadi zao, maana wewe wajibu sala zetu. Binadamu wote watakujia wewe. Tunapolemewa na makosa yetu, wewe mwenyewe watusamehe. Heri wale unaowachagua na kuwaleta karibu, waishi katika maskani yako. Sisi tutatoshelezwa na mema ya nyumba yako; mema ya hekalu lako takatifu. Kwa matendo yako makuu watuitikia na kutuokoa, ewe Mungu wa wokovu wetu; wewe ndiwe tumaini la viumbe vyote, duniani kote na mbali baharini. Kwa nguvu yako uliisimika milima mahali pake. Wewe una nguvu mno! Watuliza mshindo wa bahari na wa mawimbi yake, wakomesha ghasia za watu. Ulimwengu wote washangazwa na matendo yako. Wasababisha furaha kila mahali, toka mashariki hata magharibi. Wewe waitunza nchi kwa kuinyeshea mvua, waijalia rutuba na kuistawisha; mto wako umejaa maji tele, waifanikisha nchi na kuipatia mavuno. Hivi ndivyo uitengenezavyo nchi: Mashamba wayanyeshea mvua kwa wingi, na kuyalowanisha kwa maji; ardhi wailainisha kwa manyunyu, na kuibariki mimea ichipue. Wautunukia mwaka wote mema yako, kila ulipopitia pamejaa fanaka. Mbuga za majani zimejaa mifugo, milima nayo imejaa furaha. Malisho yamejaa kondoo, mabonde yamefunikwa kwa ngano. Kila kitu kinashangilia kwa furaha. (Kwa Mwimbishaji. Wimbo. Zaburi) Enyi watu wote duniani mshangilieni Mungu! Imbeni juu ya utukufu wa jina lake, mtoleeni sifa tukufu! Mwambieni Mungu: “Matendo yako ni ya ajabu mno! Nguvu zako ni kubwa mno hata maadui zako wanajikunyata kwa hofu. Dunia yote inakuabudu; watu wote wanakuimbia sifa!” Njoni mkaone mambo aliyotenda Mungu; ametenda mambo ya kutisha kati ya watu: Aligeuza bahari kuwa nchi kavu, watu wakapita humo kwa miguu; hapo nasi tukashangilia kwa sababu yake. Anatawala milele kwa nguvu yake kuu; macho yake huchungulia mataifa yote. Mwasi yeyote asithubutu kumpinga. Msifuni Mungu wetu, enyi mataifa yote; tangazeni sifa zake zipate kusikika. Yeye ametujalia maisha, wala hakutuacha tuanguke. Umetupima, ee Mungu, umetujaribu kama madini motoni. Umetuacha tunaswe wavuni; umetubebesha taabu nzito. Umewaacha watu watukanyage; tumepitia motoni na majini. Lakini sasa umetuleta kwenye usalama. Nitakuja nyumbani kwako na sadaka za kuteketezwa, nitakutimizia nadhiri zangu, nilizotamka na kukuahidi mimi mwenyewe nilipokuwa taabuni. Nitakutolea sadaka za kuteketezwa nononono, tambiko za kuteketezwa za kondoo madume; nitatoa sadaka za ng'ombe na mbuzi. Enyi mnaomcha Mungu, njoni nyote mkasikilize, nami nitawasimulieni aliyonitendea. Mimi nilimlilia msaada kwa sauti, sifa zake nikazitamka. Kama ningalinuia maovu moyoni, Mwenyezi-Mungu hangalinisikiliza. Lakini kweli Mungu amenisikiliza; naam, amesikiliza maneno ya sala yangu. Asifiwe Mungu, maana hakuikataa sala yangu, wala kuondoa fadhili zake kwangu. (Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi. Wimbo) Utuonee huruma, ee Mungu, utubariki; utuelekezee uso wako kwa wema; dunia yote ipate kutambua njia yako, mataifa yote yajue nguvu yako ya kuokoa. Watu wote wakutukuze, ee Mungu; watu wote na wakusifu! Mataifa yote yafurahi na kuimba kwa furaha; maana wawahukumu watu kwa haki, na kuyaongoza mataifa duniani. Watu wote wakutukuze, ee Mungu; watu wote na wakusifu! Nchi imetoa mazao yake; Mungu, Mungu wetu, ametubariki. Mungu aendelee kutubariki. Watu wote duniani na wamche. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Mungu ainuka, na maadui zake watawanyika; wanaomchukia wakimbia mbali naye! Kama moshi unavyopeperushwa na upepo, ndivyo anavyowapeperusha; kama nta inavyoyeyuka karibu na moto, ndivyo waovu wanavyoangamia mbele ya Mungu! Lakini waadilifu hufurahi ajapo Mungu, hushangilia na kuimba kwa furaha. Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake; mtengenezeeni njia yake apandaye mawinguni. Jina lake ni Mwenyezi-Mungu; furahini mbele yake. Mungu akaaye mahali pake patakatifu, ni Baba wa yatima na mlinzi wa wajane. Mungu huwapa fukara makao ya kudumu, huwafungua wafungwa na kuwapa fanaka. Lakini waasi wataishi katika nchi kame. Ee Mungu, ulipowaongoza watu wako, uliposafiri kule jangwani, dunia ilitetemeka, mbingu zilitiririsha mvua; kwa kuweko kwako, Mungu wa Sinai, naam, kwa kuweko kwako, Mungu wa Israeli! Ee Mungu, uliinyeshea nchi mvua nyingi, uliiburudisha nchi yako ilipokuwa imechakaa. Watu wako wakapata humo makao; ukawaruzuku maskini kwa wema wako. Bwana alitoa amri, nao wanawake wengi wakatangaza habari: “Wafalme na majeshi yao wanakimbia ovyo!” Kina mama majumbani waligawana nyara, ingawa walibaki mazizini: Sanamu za njiwa wa madini ya fedha, na mabawa yao yanangaa kwa dhahabu. Mungu Mwenye Nguvu alipowatawanya wafalme huko, theluji ilianguka juu ya mlima Salmoni. Ewe mlima mrefu, mlima wa Bashani, ewe mlima wa vilele vingi, mlima wa Bashani! Mbona unauonea kijicho mlima aliochagua Mungu akae juu yake? Mwenyezi-Mungu atakaa huko milele! Akiwa na msafara mkubwa, maelfu na maelfu ya magari ya kukokotwa, Bwana anakuja patakatifuni pake kutoka Sinai. Anapanda juu akichukua mateka; anapokea zawadi kutoka kwa watu, hata kutoka kwa watu walioasi; Mwenyezi-Mungu apate kukaa huko. Mwenyezi-Mungu asifiwe siku kwa siku! Yeye hutubebea mizigo yetu; yeye ndiye Mungu wa wokovu wetu. Mungu wetu ni Mungu mwenye kutuokoa; Bwana Mungu pekee ndiye aokoaye katika kifo. Mungu ataviponda vichwa vya maadui zake, naam, vichwa vya wanaoshikilia njia mbaya. Bwana alisema: “Nitawarudisha maadui kutoka Bashani; nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari, uoshe miguu katika damu ya maadui zako, nao mbwa wako wale shibe yao.” Ee Mungu, misafara yako ya ushindi yaonekana; misafara ya Mungu wangu, mfalme wangu, hadi patakatifu pake! Mbele waimbaji, nyuma wanamuziki, katikati wasichana wanavumisha vigoma. “Msifuni Mungu katika jumuiya kubwa ya watu. Msifuni Mwenyezi-Mungu, enyi wazawa wa Israeli!” Kwanza ni Benyamini, mdogo wa wote; kisha viongozi wa Yuda na kundi lao, halafu wakuu wa Zebuluni na Naftali. Onesha, ee Mungu, nguvu yako kuu; enzi yako uliyotumia kwa ajili yetu, kutoka hekaluni mwako, Yerusalemu, ambapo wafalme watakujia na zawadi zao. Uwakemee wale wanyama wakaao bwawani, kundi la mabeberu na fahali, mpaka mataifa hayo yakupe heshima na kodi. Uwatawanye hao watu wenye kupenda vita! Mabalozi watakuja kutoka Misri, Waethiopia watamletea Mungu mali zao. Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu, mwimbieni Bwana nyimbo za sifa; mwimbieni yeye apitaye katika mbingu, mbingu za kale na kale. Msikilizeni akinguruma kwa kishindo. Itambueni nguvu kuu ya Mungu; yeye atawala juu ya Israeli, enzi yake yafika katika mbingu. Mungu ni wa kutisha patakatifuni pake, naam, yeye ni Mungu wa Israeli! Huwapa watu wake nguvu na enzi. Asifiwe Mungu! (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Zaburi ya Daudi) Uniokoe, ee Mungu; maji yamenifika shingoni. Ninazama ndani ya matope makuu, hamna hata mahali pa kuweka miguu. Nimetumbukia kwenye kilindi cha maji, nachukuliwa na mawimbi. Niko hoi kwa kupiga yowe, na koo langu limekauka. Macho yangu yamefifia, nikikungojea ewe Mungu wangu. Watu wengi kuliko nywele zangu ndio wanichukiao bure. Wana nguvu sana hao wanaotaka kuniua, hao wanaonishambulia kwa mambo ya uongo. Je, nirudishe kitu ambacho sikuiba? Ee Mungu, waujua upumbavu wangu; makosa yangu hayakufichika kwako. Wanaokutumainia wasiaibishwe kwa sababu yangu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi; wanaokutafuta, wasione fedheha kwa sababu yangu ee Mungu wa Israeli. Kwa ajili yako nimefedheheshwa, aibu imefunika uso wangu. Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, kaka na dada zangu hawanitambui. Upendo wangu kwa nyumba yako unanimaliza. Kashfa zote wanazokutolea wewe zimenipata mimi. Nilipojinyenyekesha kwa kufunga, watu walinilaumu. Nilipovaa vazi la gunia kuomboleza, wao walinidharau. Watu wananisengenya mabarabarani; walevi wanatunga nyimbo juu yangu. Lakini mimi nakuomba wewe, ee Mwenyezi-Mungu; nikubalie ombi langu wakati unaopenda, ee Mungu. Kwa wingi wa fadhili zako unijibu. Wewe ni mkombozi wa kuaminika. Kwa msaada wako amini uniokoe nisizame katika matope; uniokoe na hao wanaonichukia, unisalimishe kutoka vilindi vya maji. Usiniache nikumbwe na mkondo wa maji, au nizame kwenye kilindi au nimezwe na kifo. Unijibu, ee Mwenyezi-Mungu, kwa wema na fadhili zako; unielekee kwa wingi wa huruma yako. Usimfiche mtumishi wako uso wako; unijibu haraka, maana niko hatarini. Unijie karibu na kunikomboa, uniokoe na maadui zangu wengi. Wewe wajua ninavyotukanwa, wajua aibu na kashfa ninazopata; na maadui zangu wote wewe wawajua. Kashfa zimeuvunja moyo wangu, nami nimekata tamaa. Nimetafuta kitulizo lakini sikupata, wa kunifariji lakini sikumpata. Walinipa sumu kuwa chakula, na nilipokuwa na kiu wakanipa siki. Karamu zao na ziwe mtego kwao, na sikukuu zao za sadaka ziwanase. Macho yao yatiwe giza wasiweze kuona, uitetemeshe daima migongo yao. Uwamwagie hasira yako, ghadhabu yako iwakumbe. Kambi zao ziachwe mahame, asiishi yeyote katika mahema yao. Maana wanawatesa wale uliowaadhibu, wanawaongezea majeraha wale uliowajeruhi. Uwaadhibu kwa kila uovu wao; uwakatalie kabisa msamaha wako. Uwafute katika kitabu cha walio hai, wasiwemo katika orodha ya waadilifu. Lakini mimi mnyonge na mgonjwa; uniinue juu, ee Mungu, uniokoe. Kwa wimbo nitalisifu jina la Mungu, nitamtukuza kwa shukrani. Jambo hili litampendeza Mwenyezi-Mungu zaidi, kuliko kumtolea tambiko ya ng'ombe, kuliko kumtolea fahali mzimamzima. Wanyonge wataona hayo na kufurahi; wanaomheshimu Mungu watapata moyo. Mwenyezi-Mungu huwasikiliza fukara; hatawasahau kamwe watu wake wafungwa. Enyi mbingu na dunia msifuni Mungu; bahari na vyote vilivyomo, msifuni. Maana Mungu atauokoa mji Siyoni, na kuijenga tena miji ya Yuda. Watu wake wataishi humo na kuimiliki; wazawa wa watumishi wake watairithi, wale wanaopenda jina lake wataishi humo. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi ya matoleo ya ukumbusho) Upende kuniokoa ee Mungu! Ee Mwenyezi-Mungu, uje haraka kunisaidia. Wanaonuia kuniangamiza, na waaibike na kufedheheka! Hao wanaotamani niumie, na warudi nyuma na kuaibika. Hao wanaonisimanga, na wapumbazike kwa kushindwa kwao. Lakini wote wale wanaokutafuta, wafurahi na kushangilia kwa sababu yako. Wapendao wokovu wako, waseme daima: “Mungu ni mkuu!” Nami niliye maskini na fukara, unijie haraka, ee Mungu! Ndiwe msaada wangu na mkombozi wangu; ee Mwenyezi-Mungu, usikawie! Kwako ee Mwenyezi-Mungu, nakimbilia usalama; kamwe usiniache niaibike! Kwa uadilifu wako uniokoe na kunisalimisha; unitegee sikio lako na kuniokoa! Uwe mwamba wangu wa kukimbilia usalama, ngome imara ya kuniokoa, kwani wewe ni mwamba na ngome yangu. Niokoe, ee Mungu wangu, mikononi mwa waovu, kutoka makuchani mwa wabaya na wakatili. Maana wewe Bwana u tumaini langu; tegemeo langu ee Mwenyezi-Mungu, tangu ujana wangu; nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu, ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu. Mimi nitakusifu wewe daima. Kwa wengi nimekuwa kioja, lakini wewe u kimbilio langu imara. Kinywa changu kimejaa sifa zako, na utukufu wako mchana kutwa. Wakati wa uzee usinitupe; niishiwapo na nguvu usiniache. Maana maadui zangu wanasema vibaya juu yangu; wanaovizia uhai wangu wanafanya mipango, na kusema: “Mungu amemwacha; mfuateni na kumkamata, kwani hakuna wa kumwokoa!” Usikae mbali nami, ee Mungu; uje haraka kunisaidia, ee Mungu wangu. Wapinzani wangu wote waaibishwe na kuangamizwa; wenye kutaka kuniumiza wapate aibu na fedheha. Lakini mimi nitakuwa na matumaini daima; tena nitakusifu zaidi na zaidi. Kinywa changu kitatamka matendo yako ya haki, nitatangaza mchana kutwa matendo yako ya wokovu ijapokuwa hayo yanapita akili zangu. Nitataja matendo yako makuu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu; nitatangaza kuwa ndiwe mwadilifu peke yako. Ee Mungu, wewe umenifunza tangu ujana wangu; tena na tena, natangaza matendo yako ya ajabu. Usiniache, ee Mungu, niwapo mzee mwenye mvi, hata nivitangazie vizazi vijavyo nguvu yako. Nguvu na uadilifu wako, ee Mungu, vyafika mpaka mbingu za juu. Wewe umefanya mambo makuu mno. Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe? Umenifanya nione taabu nyingi ngumu, lakini utanirudishia tena uhai, wewe utaniinua tena kutoka huko chini. Utaniongezea heshima yangu, na kunifariji tena. Nitakusifu pia kwa kinubi, kwa sababu ya uaminifu wako, ee Mungu wangu; nitakuimbia sifa kwa zeze, ewe Mtakatifu wa Israeli. Nitapaza sauti kwa furaha, ninapokuimbia wewe sifa zako, na roho yangu itakusifu maana umeniokoa. Nitatamka uadilifu wako mchana kutwa, maana waliotaka kuniumiza wameaibishwa na kufedheheshwa. (Zaburi ya Solomoni) Ee Mungu, umjalie mfalme uamuzi wako, umpe mwanamfalme uadilifu wako; atawale taifa lako kwa haki, na maskini wako kwa uadilifu. Milima ilete fanaka kwa watu wako, vilima vijae uadilifu. Mfalme awatetee wanyonge wa taifa, awasaidie watoto wa fukara, na kuwaangamiza watu wadhalimu. Mfalme aishi muda mrefu kama jua, na kama mwezi, kwa vizazi vyote. Awe kama manyunyu yaburudishayo mashamba, kama mvua iinyweshayo ardhi. Uadilifu ustawi maisha yake yote, na amani kwa wingi mpaka mwezi ukome. Atawale kutoka bahari hata bahari, kutoka mto Eufrate hata mipaka ya dunia. Maadui zake wakaao nyikani wanyenyekee mbele yake, washindani wake walambe vumbi. Wafalme wa Tarshishi na visiwa wamlipe kodi, wafalme wa Sheba na Seba wamletee zawadi. Wafalme wote wa dunia wamheshimu, watu wa mataifa yote wamtumikie. Anamkomboa fukara anayemwomba, na maskini asiye na wa kumsaidia. Anawahurumia watu dhaifu na fukara, anayaokoa maisha yao wenye shida. Anawatoa katika udhalimu na ukatili, maana maisha yao ni ya thamani kubwa kwake. Mfalme na aishi maisha marefu; apokee zawadi ya dhahabu kutoka Sheba; watu wamwombee kwa Mungu daima, na kumtakia baraka mchana kutwa. Nchi na izae nafaka kwa wingi, vilima vijae mavuno kama ya Lebanoni, na watu mijini wastawi kama nyasi. Jina la mfalme litukuke daima; fahari yake idumu pindi liangazapo jua. Kwake mataifa yote yabarikiwe; watu wote wamwite mbarikiwa! Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye peke yake hufanya miujiza. Jina lake tukufu na litukuzwe milele; utukufu wake ujae ulimwenguni kote! Amina, Amina! Mwisho wa sala za Daudi, mwana wa Yese. (Zaburi ya Asafu) Hakika, Mungu ni mwema kwa watu wanyofu; ni mwema kwa walio safi moyoni. Karibu sana ningejikwaa, kidogo tu ningeteleza; maana niliwaonea wivu wenye kiburi, nilipoona wakosefu wakifanikiwa. Maana hao hawapatwi na mateso; miili yao ina afya na wana nguvu. Taabu za binadamu haziwapati hao; hawapati mateso kama watu wengine. Kiburi kimekuwa mkufu wao shingoni, uhasama ni kama nguo yao. Macho yao hufura kwa uovu; mioyo yao hububujika mipango mibaya. Huwadhihaki wengine na kusema mabaya; hujivuna na kupanga kufanya uhasama. Kwa vinywa vyao hutukana mbingu; kwa ndimi zao hujitapa duniani. Hata watu wa Mungu wanawafuata, hawaoni kwao chochote kibaya na kusadiki kila wanachosema. Wanasema: “Mungu hawezi kujua! Mungu Mkuu hataweza kugundua!” Hivi ndivyo watu waovu walivyo; wana kila kitu na wanapata mali zaidi. Je, nimetunza bure usafi moyoni, na kujilinda nisitende dhambi? Mchana kutwa nimepata mapigo, kila asubuhi nimepata mateso. Kama ningalisema hayo kama wao, ningalikuwa mhaini miongoni mwa watu wako. Basi, nilijaribu kufikiria jambo hili, lakini lilikuwa gumu mno kwangu, mpaka nilipoingia patakatifu pako. Ndipo nikatambua yatakayowapata waovu. Kweli wewe wawaweka mahali penye utelezi; wawafanya waanguke na kuangamia. Wanaangamizwa ghafla, na kufutiliwa mbali kwa vitisho. Ee Bwana, uinukapo, wao hutoweka mara, kama ndoto wakati mtu anapoamka asubuhi. Nilipoona uchungu moyoni na kuchomwa rohoni, nilikuwa mpumbavu na mjinga, nilikuwa kama mnyama mbele yako. Hata hivyo niko daima nawe, ee Mungu! Wanishika mkono na kunitegemeza. Wewe waniongoza kwa mashauri yako; mwishowe utanipokea kwenye utukufu. Mbinguni, nani awezaye kunisaidia ila wewe? Na duniani hamna ninachotamani ila wewe! Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni, wewe, ee Mungu, u mwamba wangu; riziki yangu kuu ni wewe milele. Anayejitenga nawe, hakika ataangamia. Anayekukana, utamwangamiza. Lakini, kwangu ni vema kuwa karibu na Mungu, wewe Bwana Mwenyezi-Mungu ndiwe usalama wangu. Nitatangaza mambo yote uliyotenda! (Utenzi wa Asafu) Kwa nini, ee Mungu, umetutupa kabisa? Mbona hasira yako inawaka dhidi ya kondoo wako! Kumbuka jumuiya yako uliyojipatia tangu kale, kabila ulilolikomboa liwe mali yako, kumbuka mlima Siyoni mahali unapokaa. Pita juu ya magofu haya ya kudumu! Adui wameharibu kila kitu hekaluni. Maadui zako wamenguruma ushindi hekaluni mwako! Wameweka humo bendera zao za ushindi! Wanafanana na mtema kuni, anayekata miti kwa shoka lake. Waliivunjavunja milango ya hekalu, kwa mashoka na nyundo zao. Walichoma moto patakatifu pako; walikufuru mahali pale unapoheshimiwa. Walipania kutuangamiza sote pamoja; walichoma kila mahali tulipokutania kukuabudu nchini. Hatuzioni tena ishara zetu takatifu, hatuna tena nabii yeyote! Hata hatujui yatakuwa hivi hadi lini! Mpaka lini, ee Mungu, adui atakucheka? Je, watalikufuru jina lako milele? Mbona umeuficha mkono wako? Kwa nini hunyoshi mkono wako? Hata hivyo wewe Mungu ni mfalme wetu tangu kale; umefanya makuu ya wokovu katika nchi. Kwa enzi yako kuu uliigawa bahari; uliviponda vichwa vya majoka ya bahari. Wewe uliviponda vichwa vya dude Lewiyathani; ukawapa wanyama wa jangwani mzoga wake. Wewe umefanya chemchemi na vijito; na kuikausha mito mikubwa. Mchana ni wako na usiku ni wako; umeweka mwezi na jua mahali pao. Wewe umeweka mipaka yote ya dunia; umepanga majira ya kiangazi na ya baridi. Kumbuka, ee Mwenyezi-Mungu, madharau ya maadui zako; taifa pumbavu linalikashifu jina lako. Sisi ni dhaifu kama njiwa. Usiwatupie wanyama wakali uhai wa wapenzi wako; usiyasahau maisha ya maskini wako. Ulikumbuke agano ulilofanya nasi! Nchi imejaa uharamia kila mahali pa giza. Usiwaache wanaokandamizwa waaibishwe, uwajalie maskini na wahitaji walisifu jina lako. Inuka, ee Mungu, ukajitetee; ukumbuke wanavyokudharau kila siku watu wasiokujua. Usisahau makelele za maadui zako; na ghasia za daima za wapinzani wako. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Usiharibu”. Zaburi ya Asafu. Wimbo) Tunakushukuru, ee Mungu, tunakushukuru! Tunatangaza ukuu wa jina lako na kusimulia juu ya matendo yako makuu. Mungu asema: “Mimi nimeweka wakati maalumu! Wakati huo nitahukumu kwa haki. Nchi ikitetemeka na vyote vilivyomo, mimi ndiye ninayeitegemeza misingi yake. Nawaambia wenye kiburi: ‘Acheni kujigamba’; na waovu: ‘Msioteshe pembe za kiburi! Msijione kuwa watu wa maana sana, wala kusema maneno ya majivuno.’” Hukumu haitoki mashariki au magharibi; wala haitoki nyikani au mlimani. Mungu mwenyewe ndiye hakimu; humshusha mmoja na kumkweza mwingine. Mwenyezi-Mungu, anashika kikombe mkononi, kimejaa divai kali ya hasira yake; anaimimina na waovu wote wanainywa; naam, wanainywa mpaka tone la mwisho. Lakini mimi nitafurahi milele, nitamwimbia sifa Mungu wa Yakobo. Atavunja nguvu zote za watu waovu; lakini nguvu za waadilifu ataziimarisha. (Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Asafu. Wimbo) Mungu anajulikana katika Yuda; jina lake ni kuu katika Israeli. Makao yake yamo huko Salemu; maskani yake huko Siyoni. Huko alivunja mishale ya adui; alivunja ngao, panga na silaha za vita. Wewe, ee Mungu, watukuka mno; umejaa fahari kuliko milima ya milele. Wenye nguvu walipokonywa nyara zao, sasa wamelala usingizi wa kifo, mashujaa wa vita hawakuweza kutumia mikono yao. Ulipowakemea, ee Mungu wa Yakobo, farasi na wapandafarasi walikufa ganzi. Wewe, ee Mungu, ni wa kutisha mno! Nani awezaye kustahimili mbele yako ukikasirika? Ulijulisha hukumu yako toka mbinguni; dunia iliogopa na kunyamaza; wakati ulipoinuka kutekeleza hukumu, kuwaokoa wote wanaodhulumiwa duniani. Ghadhabu ya watu husababisha tu sifa kwako; na waliookoka vitani watafanya sikukuu zako. Mtimizieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ahadi zenu; enyi mlio karibu mpeni zawadi Mungu wa kutisha. Yeye huzitoa roho za wakuu; huwatisha wafalme wa dunia. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Asafu) Namlilia Mungu kwa sauti, kwa sauti namlilia Mungu anisikie. Wakati wa taabu namwomba Bwana; namnyoshea mikono yangu usiku bila kuchoka, lakini sipati faraja yoyote kwa mtu. Ninamfikiria Mungu na kusononeka; ninatafakari na kufa moyo. Wanizuia hata kupata lepe la usingizi, nina mahangaiko hata kusema siwezi. Nafikiria siku za zamani; nakumbuka miaka ya hapo kale. Usiku nawaza na kuwazua moyoni; natafakari na kujiuliza rohoni: “Je, Bwana ametuacha kabisa? Je, hatatuonesha tena hisani yake? Je fadhili zake zimekoma kabisa? Je, hatatimiza tena ahadi zake? Je, Mungu amesahau kuwa na huruma? Je, hasira yake imeuondoa upole wake?” Kisha nikasema, “Kinachonichoma zaidi ni kwamba, Mungu Mkuu hatendi tena kitu kwa ajili yetu!” Nitayakumbuka matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, naam, nitayafikiria maajabu yako ya hapo kale. Nitatafakari juu ya kazi zako, na kuwaza juu ya matendo yako makuu. Kila ufanyacho ee Mungu, ni kitakatifu. Ni mungu gani aliye mkuu kama Mungu wetu? Wewe ni Mungu unayetenda maajabu; wewe umeyaonesha mataifa uwezo wako. Kwa mkono wako wa nguvu uliwakomboa watu wako; uliwakomboa wazawa wa Yakobo na Yosefu. Maji yalipokuona, ee Mungu, maji yalipokuona, yaliogopa mno; naam, bahari ilitetemeka hata vilindini. Mawingu yalichuruzika maji, ngurumo zikavuma angani, mishale ya umeme ikaangaza kila upande. Kishindo cha ngurumo yako kilitokea katika kimbunga, umeme wako ukauangaza ulimwengu; dunia ikatikisika na kutetemeka. Wewe uliweka njia yako juu ya bahari; ulitembea juu ya maji yale mengi, lakini nyayo zako hazikuonekana. Uliwaongoza watu wako kama kondoo, chini ya uongozi wa Mose na Aroni. (Utenzi wa Asafu) Sikieni mafundisho yangu, enyi watu wangu; yategeeni sikio maneno ya kinywa changu. Nitasema nanyi kwa mafumbo, nitasema mambo yaliyofichika tangu kale; mambo tuliyoyasikia na kuyajua, mambo ambayo wazee wetu walitusimulia. Hatutawaficha watoto wetu; ila tutakisimulia kizazi kijacho matendo matukufu ya Mwenyezi-Mungu na uwezo wake; tutawaambia maajabu yake aliyotenda. Aliwapa wazawa wa Yakobo masharti, aliweka sheria katika Israeli, ambayo aliwaamuru wazee wetu wawafundishe watoto wao; ili watu wa kizazi kijacho, watoto watakaozaliwa baadaye, wazijue, nao pia wawajulishe watoto wao, ili wamwekee Mungu tumaini lao, wasije wakasahau matendo ya Mungu, bali wazingatie amri zake. Wasiwe kama walivyokuwa wazee wao, watu wakaidi na waasi; kizazi ambacho hakikuwa na msimamo thabiti, ambacho hakikuwa na uaminifu kwa Mungu. Watu wa Efraimu, pinde na mishale mkononi, walirudi nyuma, wakakimbia siku ile ya vita. Hawakulizingatia agano la Mungu; walikataa kufuata sheria yake. Walisahau mambo aliyokuwa ametenda, miujiza aliyokuwa amewaonesha. Alifanya maajabu mbele ya wazee wao, kondeni Soani, nchini Misri. Aliigawa bahari, akawapitisha humo; aliyafanya maji yasimame kama ukuta. Mchana aliwaongoza kwa wingu; usiku kucha kwa mwanga wa moto. Aliipasua miamba kule jangwani, akawanywesha maji kutoka vilindini. Alibubujisha vijito kutoka mwambani, akatiririsha maji kama mito. Hata hivyo waliendelea kumkosea Mungu; walimwasi Mungu Mkuu kule jangwani. Walimjaribu Mungu kwa makusudi; wakidai wapewe chakula walichotaka. Walimkufuru Mungu wakisema: “Je, Mungu aweza kutupa chakula jangwani? Ni kweli, aliupiga mwamba, maji yakabubujika kama mto; lakini, sasa aweza kweli kutupatia mkate, na kuwapatia watu wake nyama?” Mwenyezi-Mungu, aliposikia hayo, alijawa na ghadhabu, moto ukawawakia wazawa wa Yakobo; hasira yake ikawavamia watu wa Israeli, kwa sababu hawakuwa na imani naye, wala hawakuamini nguvu yake ya kuokoa. Hata hivyo aliyaamuru mawingu ya juu, akaifungua milango ya mbingu; akawanyeshea mana wale, akawapa nafaka kutoka mbinguni. Binadamu, wakala chakula cha malaika; naye aliwapelekea chakula cha kutosha. Alivumisha upepo wa mashariki, kwa nguvu yake akachochea pepo za kusini; akawanyeshea watu wake nyama kama vumbi, ndege wengi kama mchanga wa pwani; ndege hao walianguka kambini mwao, kila mahali kuzunguka makao yao. Watu walikula wakashiba; Mungu aliwapa walichotaka. Lakini hata kabla ya kutosheleza hamu yao, chakula kikiwa bado mdomoni mwao, hasira ya Mungu iliwaka juu yao; akawaua wenye nguvu miongoni mwao, na kuwaangusha vijana wa Israeli. Hata hivyo waliendelea kumkosea Mungu; ijapokuwa alitenda maajabu, hawakuamini. Basi, akazikatisha siku zao kama pumzi, miaka yao kwa maafa ya ghafla. Kila alipowaua, waliobaki walimgeukia; walitubu, wakamgeukia Mungu kwa moyo. Walikumbuka kwamba Mungu alikuwa mwamba wao; Mungu Mkuu alikuwa mkombozi wao. Lakini walimdanganya kwa maneno yao; kila walichomwambia kilikuwa uongo. Hawakuambatana naye kwa moyo, hawakuwa waaminifu kwa agano lake. Lakini Mungu mwenye huruma alisamehe uovu wao, na wala hakuwaangamiza. Mara nyingi aliizuia hasira yake, wala hakuiacha ghadhabu yake yote iwake. Alikumbuka kwamba wao ni watu tu; ni kama upepo upitao na kutoweka. Mara ngapi walimwasi kule jangwani, na kumchukiza hukohuko nyikani! Walimjaribu Mungu tena na tena, wakamkasirisha huyo Mtakatifu wa Israeli. Hawakuikumbuka nguvu yake, wala siku ile alipowaokoa na maadui zao, alipotenda maajabu nchini Misri, na miujiza kondeni Soani! Aliigeuza ile mito kuwa damu, Wamisri wasipate maji ya kunywa. Aliwapelekea makundi ya nzi waliowasumbua, na vyura waliowatia hasara. Alituma nzige, wakala mavuno yao, na kuharibu mashamba yao. Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, na mitini yao kwa baridi kali. Ngombe wao aliwaua kwa mvua ya mawe, na kondoo wao kwa radi. Aliacha hasira yake kali iwawakie, ghadhabu, chuki na dhiki, na kundi la malaika waangamizi. Aliachilia hasira yake iendelee, wala hakuwaepusha na kifo, bali aliwaangamiza kwa tauni. Aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Wamisri; naam, chipukizi wa kwanza kambini mwa Hamu. Kisha aliwahamisha watu wake kama kondoo, akawaongoza jangwani kama kundi la mifugo. Aliwaogoza salama, wala hawakuogopa; lakini bahari iliwafunika maadui zao. Aliwaleta katika nchi yake takatifu, katika mlima aliouteka kwa nguvu yake. Aliyafukuza mataifa mbele yao, akazitoa nchi zao ziwe mali ya Israeli, akayakalisha makabila ya Israeli mahemani mwao. Hata hivyo walimjaribu na kumwasi Mungu Mkuu; wala hawakuzingatia masharti yake. Ila waligeuka na kufanya mabaya kama wazee wao; wakayumbayumba kama upinde usio imara. Walimkasirisha kwa madhabahu zao za miungu; wakamchochea aone wivu kwa sanamu zao za kuchonga. Mungu alipoona hayo, akawaka hasira; akamkataa Israeli katakata. Aliyaacha makao yake kule Shilo, makao ambamo alikaa kati ya watu. Aliiacha ishara ya nguvu yake itekwe, utukufu wake utiwe mikononi mwa maadui. Aliwakasirikia watu wake mwenyewe; akawatoa waangamizwe kwa upanga. Moto ukawateketeza vijana wao wa kiume, na wasichana wao wakakosa wachumba. Makuhani wao walikufa kwa upanga, wala wajane wao hawakuomboleza. Kisha Bwana aliamka kama kutoka usingizini, kama shujaa aliyechangamshwa na divai. Akawatimua maadui zake; akawatia aibu ya kudumu milele. Lakini aliikataa jamaa ya Yosefu, wala hakulichagua kabila la Efraimu. Ila alilichagua kabila la Yuda, mlima Siyoni anaoupenda. Alijenga hapo hekalu lake kubwa kama mbingu, kama dunia aliyoiweka imara milele. Alimchagua Daudi, mtumishi wake, akamtoa katika kazi ya kuchunga kondoo. Alimtoa katika kazi ya kuchunga kondoo na wanakondoo, awe na jukumu la kuchunga watu wa Yakobo taifa lake. Achunge Israeli, watu wake Mungu mwenyewe. Daudi akawafunza kwa moyo wake wote, akawaongoza kwa uhodari mkubwa. (Zaburi ya Asafu) Ee Mungu, watu wasiokujua wameivamia nchi yako. Wamelitia najisi hekalu lako takatifu, na kuufanya mji wa Yerusalemu kuwa magofu. Wameacha maiti za watumishi wako ziliwe na ndege, miili ya watu wako chakula cha wanyama wa porini. Damu yao imemwagwa kama maji mjini Yerusalemu, wamelazwa humo na hakuna wa kuwazika. Tumekuwa aibu kwa mataifa ya jirani, jirani zetu wanatucheka na kutudhihaki. Ee Mwenyezi-Mungu, je, utakasirika hata milele? Hasira yako ya wivu itawaka kama moto hata lini? Uwamwagie watu wasiokujua hasira yako; naam, tawala zote zisizoheshimu jina lako. Maana wamemmeza Yakobo, taifa lako, wameteketeza kabisa makao yake. Usituadhibu kwa sababu ya makosa ya wazee wetu. Huruma yako itujie haraka, maana tumekandamizwa mno! Utusaidie, ee Mungu, mwokozi wetu; kwa heshima ya jina lako utuokoe na kutusamehe dhambi zetu, kwa ajili ya jina lako. Kwa nini mataifa yatuambie: “Yuko wapi Mungu wenu?” Utujalie tuone ukiwalipiza watu wa mataifa mauaji ya watumishi wako. Kilio cha hao wafungwa kikufikie; kwa nguvu yako kuu uwaokoe waliohukumiwa kufa. Mataifa hayo yaliyokudharau, ee Bwana, yalipizwe mara saba! Nasi watu wako, tulio kondoo wa kundi lako, tutakushukuru milele, na kukusifu nyakati zote. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Zaburi ya Asafu) Utege sikio, ewe Mchungaji wa Israeli, uwaongozaye wazawa wa Yosefu kama kondoo. Ewe ukaaye juu ya viumbe vyenye mabawa, uangaze, mbele ya Efraimu, Benyamini na Manase. Uoneshe nguvu yako, uje kutuokoa! Uturekebishe, ee Mungu; utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, hata lini utazikasirikia sala za watu wako? Umefanya huzuni iwe chakula chetu; umetunywesha machozi kwa wingi. Umetufanya tuwe dharau kwa jirani zetu; maadui zetu wanatudhihaki. Ee Mungu wa majeshi, uturekebishe, utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka. Ulileta mzabibu kutoka Misri; ukawafukuza watu wa mataifa mengine, na kuupanda katika nchi yao. Uliupalilia upate kukua, nao ukatoa mizizi na kuenea kote nchini. Uliifunika milima kwa kivuli chake, na matawi yake yakawa kama mierezi mikubwa. Matawi yake yalienea mpaka baharini; machipukizi yake mpaka kando ya mto Eufrate. Mbona ulibomoa kuta zilizouzunguka? Sasa kila apitaye anachuma zabibu zake; nguruwe mwitu wanauharibu, na wanyama wa porini wanautafuna! Utugeukie tena ee Mungu wa majeshi. Uangalie toka mbinguni, uone; ukautunze mzabibu huo. Uulinde mche ulioupanda kwa mkono wako; hilo chipukizi uliloimarisha wewe mwenyewe. Watu walioukata na kuuteketeza, uwatazame kwa ukali, waangamie. Mkono wako umkinge huyo uliyemfadhili; huyo uliyemteua kwa ajili yako. Hatutakuacha na kukuasi tena; utujalie uhai, nasi tutakusifu. Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi uturekebishe; utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Gitithi. Zaburi ya Asafu) Mwimbieni kwa sauti Mungu, nguvu yetu, mshangilieni Mungu wa Yakobo; vumisheni wimbo wa shangwe, pigeni ngoma, chezeni zeze na kinubi cha sauti nzuri. Pigeni tarumbeta kutangaza mwezi mwandamo, na pia mwezi mpevu, wakati wa sikukuu yetu. Hiyo ndiyo kanuni katika Israeli; hilo ndilo agizo la Mungu wa Yakobo. Aliwapa watu wa Israeli agizo hilo, alipoishambulia nchi ya Misri. Nasikia sauti nisiyoitambua ikisema: “Mimi nilikutua mizigo yako mabegani, nilikuondolea matofali uliyochukua mikononi. Ukiwa shidani uliniita, nami nikakuokoa. Nilikujibu nikiwa mafichoni katika ngurumo. Nilikujaribu kwenye maji ya Meriba. Enyi watu wangu, sikieni onyo langu. Laiti ungenisikiliza, ee Israeli! Asiwepo kwako mungu wa kigeni; usiabudu kamwe mungu mwingine. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri. Fumbua kinywa chako, nami nitakulisha. “Lakini watu wangu hawakunisikiliza; Israeli hakunitaka kabisa. Hivyo, nikawaacha wabaki na ukaidi wao; wafuate mashauri yao wenyewe. Laiti watu wangu wangenisikiliza! Laiti Israeli angefuata njia yangu! Ningewashinda maadui zao haraka; ningenyosha mkono dhidi ya wadhalimu wao. Wanichukiao wangenipigia magoti kwa hofu, na adhabu yao ingekuwa ya milele. Lakini wewe ningekulisha kwa ngano bora, ningekushibisha kwa asali ya mwambani.” (Zaburi ya Asafu) Mungu anasimamia baraza lake; anatoa hukumu katika kusanyiko la miungu: “Mpaka lini mtaendelea kuhukumu bila haki na kuwapendelea watu waovu? Wapeni wanyonge na yatima haki zao; tekelezeni haki za wanaoonewa na fukara. Waokoeni wanyonge na maskini, waokoeni makuchani mwa wadhalimu. “Lakini nyinyi hamjui wala hamfahamu! Nyinyi mnatembea katika giza la upotovu! Misingi yote ya haki duniani imetikiswa! Mimi nilisema kuwa nyinyi ni miungu; kwamba nyote ni watoto wa Mungu Mkuu! Hata hivyo, mtakufa kama watu wote; mtaanguka kama mkuu yeyote.” Inuka ee Mungu, uuhukumu ulimwengu; maana mataifa yote ni mali yako. (Zaburi ya Asafu. Wimbo) Ee Mungu, usikae kimya! Usinyamaze ee Mungu, wala usitulie! Tazama! Maadui zako wanafanya ghasia; wanaokuchukia wanainua vichwa kwa kiburi. Wanapanga kwa hila kuwadhuru watu wako; wanashauriana dhidi ya hao unaowalinda. Wanasema: “Njoni tuliangamize taifa lao, jina la Israeli lisikumbukwe tena.” Naam, wanakubaliana kwa moyo mmoja, wanakula kiapo dhidi yako: Watu wa Edomu na Waishmaeli, Wamoabu na watu wa Hagari; watu wa Gebali, Amoni na Amaleki, watu wa Filistia na wakazi wa Tiro. Hata Ashuru imeshirikiana nao, imewaunga mkono wazawa wa Loti! Uwatende ulivyowatenda watu wa Midiani, ulivyowatenda Sisera na Yabini mtoni Kishoni, watu uliowaangamiza kule Endori, wakawa takataka juu ya nchi. Uwatende wakuu wao kama Orebu na Zeebu; watawala wao wote kama Zeba na Zalmuna, ambao walisema: “Tutajitekea nchi ya Mungu.” Ee Mungu wangu, uwafanye kama vumbi; kama makapi yapeperushwayo na upepo. Kama vile moto unavyoteketeza msitu, na miali ya moto inavyounguza milima, uwakimbize hao kwa tufani yako, na kuwatisha kwa kimbunga chako! Uzijaze nyuso zao fedheha, wapate kukutafuta, ee Mwenyezi-Mungu. Waone fedheha na kuhangaika milele, waangamie kwa aibu kabisa. Wajue kwamba wewe peke yako ambaye jina lako ni Mwenyezi-Mungu, ndiwe Mungu Mkuu juu ya dunia yote. (Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Gitithi. Zaburi ya Wakorahi) Jinsi gani yanavyopendeza makao yako, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi! Nafsi yangu yatamani mno maskani ya Mwenyezi-Mungu! Moyo na mwili wangu wote wamshangilia Mungu aliye hai. Hata shomoro wamepata makao yao, mbayuwayu wamejenga viota vyao, humo wameweka makinda yao, katika madhabahu zako, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu! Heri wale wanaokaa nyumbani mwako, wakiimba daima sifa zako. Heri watu wanaopata nguvu zao kwako, wanaotamani kwenda kuhiji mlimani kwako. Wapitapo katika bonde kavu la Baka, hulifanya kuwa mahali pa chemchemi, na mvua za vuli hulijaza madimbwi. Wanaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi; watamwona Mungu wa miungu huko Siyoni. Usikie sala yangu ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi; unitegee sikio, ee Mungu wa Yakobo. Ee Mungu, umwangalie kwa wema ngao yetu mfalme, umtazame huyo uliyemweka wakfu kwa mafuta. Siku moja tu katika maskani yako, ni bora kuliko siku elfu mahali pengine; afadhali kusimama mlangoni pa nyumba yako, kuliko kuishi nyumbani kwa watu waovu. Mwenyezi-Mungu ni jua letu na ngao yetu; yeye hutuneemesha na kutujalia fahari. Hawanyimi chochote kilicho chema, wale waishio kwa unyofu. Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, heri mtu yule anayekutumainia wewe! (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi) Ee Mwenyezi-Mungu, umeifadhili nchi yako; umemjalia Yakobo bahati nzuri tena. Umewasamehe watu wako kosa lao; umezifuta dhambi zao zote. Umeizuia ghadhabu yako yote; umeiacha hasira yako kali. Uturekebishe tena, ee Mungu mwokozi wetu; uiondoe chuki uliyo nayo juu yetu. Je, utatukasirikia hata milele? Je, utadumisha ghadhabu yako kwa vizazi vyote? Je, hutatujalia tena maisha mapya, ili watu wako wafurahi kwa sababu yako? Utuoneshe, fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, utujalie wokovu wako. Hebu nisikie anachosema Mwenyezi-Mungu; maana anaahidi kuwapa watu wake amani, watu wake mwenyewe wasiporudia upuuzi wao Hakika yu tayari kuwaokoa wanaomheshimu, na utukufu wake utadumu nchini mwetu. Fadhili zake na uaminifu vitakutana; uadilifu na amani vitaungana. Uaminifu utachipuka katika nchi; uadilifu utashuka toka mbinguni. Naam, Mwenyezi-Mungu atatuletea fanaka, na nchi yetu itatoa mazao yake mengi. Uadilifu utamtangulia Mungu na kumtayarishia njia yake. (Sala ya Daudi) Unitegee sikio, ee Mwenyezi-Mungu, unijibu, maana mimi ni fukara na mnyonge. Uyahifadhi maisha yangu maana mimi ni mchaji wako; uniokoe mimi mtumishi wako ninayekutegemea. Wewe ni Mungu wangu; basi, unionee huruma, maana nakulilia mchana kutwa. Uifurahishe roho yangu mimi mtumishi wako, maana sala zangu nazielekeza kwako ee Bwana. Wewe, ee Bwana, u mwema na mwenye kusamehe; mwingi wa fadhili kwa wote wakuombao. Ee Mwenyezi-Mungu, uitegee sikio sala yangu; ukisikie kilio cha ombi langu. Siku za taabu nakuita, maana wewe waniitikia. Ee Bwana, hakuna Mungu aliye kama wewe; hakuna awezaye kufanya unayofanya wewe. Mataifa yote uliyoyaumba, yatakuja kukuabudu, ee Bwana; yatatangaza ukuu wa jina lako. Wewe ndiwe mkuu, wafanya maajabu; wewe peke yako ndiwe Mungu. Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu, nipate kuwa mwaminifu kwako; uongoze moyo wangu nikuheshimu. Ee Bwana, Mungu wangu, nitakusifu kwa moyo wote; nitatangaza ukuu wa jina lako milele. Fadhili zako kwangu ni nyingi mno! Umeniokoa kutoka chini kuzimu. Ee Mungu, watu wenye kiburi wamenikabili; kundi la watu wakatili wanataka kuniua, wala hawakujali wewe hata kidogo. Lakini wewe Bwana, ni Mungu wa rehema na huruma; wewe ni mvumilivu, mwingi wa fadhili na uaminifu. Unigeukie, unihurumie; unijalie nguvu yako mimi mtumishi wako, umwokoe mtoto wa mjakazi wako. Unioneshe ishara ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu, ili wale wanaonichukia waaibike, waonapo umenisaidia na kunifariji. (Zaburi ya Wakorahi. Wimbo) Mungu amejenga mji wake juu ya mlima wake mtakatifu. Mwenyezi-Mungu anaupenda mji wa Siyoni, kuliko makao mengine ya Yakobo. Mambo ya fahari yanasemwa juu yako, ee mji wa Mungu: “Miongoni mwa wale wanijuao mimi, wapo watu wa Misri na Babuloni. Kadhalika Filistia, Tiro na Kushi, wote walizaliwa kwako!” Na kuhusu Siyoni itasemwa: “Siyoni ni mama wa huyu na huyu; Mungu Mkuu atauthibitisha.” Mwenyezi-Mungu ataandika katika kitabu, atakapoorodhesha watu: “Huyu amezaliwa huko!” Wote wanacheza ngoma na kuimba: “Siyoni, chanzo chetu ni kwako.” (Wimbo. Zaburi ya Wakorahi. Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Mahalathi Nealothi. Utenzi wa Hemani Mwezrahi) Ee Mwenyezi-Mungu, mwokozi wangu, ninalia mchana kutwa, na usiku nakulalamikia. Sala yangu ikufikie, usikilize kilio changu. Maafa mengi yamenipata, nami niko karibu kufa. Ninaonekana kama mtu anayekufa, nguvu zangu zote zimeniishia. Nimesahauliwa kati ya wafu, kama waliouawa, walioko kaburini; kama wale ambao huwakumbuki tena, ambao wametengwa na ulinzi wako. Umenitupa katika kina cha kaburi; katika sehemu za giza na kina kikuu. Hasira yako imenilemea; umenisonga kwa mawimbi yako yote. Umewafanya rafiki zangu waniepe, umenifanya kuwa chukizo kwao. Nimefungwa ndani, wala siwezi kutoroka; macho yangu yamefifia kwa huzuni. Kila siku nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu; ninakunyoshea mikono yangu. Je, wewe huwatendea wafu maajabu yako? Je, mizimu hufufuka na kukusifu? Je, fadhili zako zinatajwa kaburini, au uaminifu wako kwenye makao ya maangamizi? Je, maajabu yako yanajulikana humo gizani, au wema wako katika nchi ya waliosahauliwa? Lakini mimi nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu; kila asubuhi nakuletea ombi langu. Mbona ee Mwenyezi-Mungu wanitupilia mbali? Kwa nini unanificha uso wako? Nimeteseka na kukaribia kifo tangu ujana wangu; nateseka kwa mapigo yako, niko hoi kabisa. Ghadhabu yako imeniwakia; mashambulio yako ya kutisha yananiangamiza. Yananizunguka kama mafuriko mchana kutwa; yananizingira yote kwa pamoja. Umewafanya rafiki na wenzangu wote waniepe; giza ndilo limekuwa mwenzangu. (Utenzi wa Ethani Mwezrahi) Ee Mwenyezi-Mungu, nitaimba fadhili zako milele; nitavitangazia vizazi vyote uaminifu wako. Natamka kuwa fadhili zako zadumu milele; uaminifu wako ni thabiti kama mbingu. Umesema: “Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia mtumishi wangu Daudi: ‘Daima nitamweka mzawa wako kuwa mfalme, tena nitaudumisha ufalme wako milele.’” Mbingu na zisifu maajabu yako, ee Mwenyezi-Mungu; uaminifu wako usifiwe katika kusanyiko la watakatifu. Nani mbinguni awezaye kulinganishwa nawe ee Mwenyezi-Mungu? Nani aliye sawa nawe kati ya viumbe vya mbinguni? Wewe waogopwa katika baraza la watakatifu; wote wanaokuzunguka wanatiwa hofu kuu. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, ni nani mwenye nguvu kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu? Uaminifu umekuzunguka pande zote. Wewe watawala machafuko ya bahari; mawimbi yake yakiinuka, wayatuliza. Uliliponda joka Rahabu na kuliua; uliwatawanya adui zako kwa nguvu yako. Mbingu ni zako na dunia ni yako pia; ulimwengu na vitu vyote vilivyomo wewe uliviumba. Wewe uliumba kaskazini na kusini; milima Tabori na Hermoni inakusifu kwa furaha. Mkono wako una nguvu, mkono wako una nguvu na umeshinda! Uadilifu na haki ni msingi wa utawala wako; fadhili na uaminifu vyakutangulia! Heri watu wanaojua kukushangilia, wanaoishi katika mwanga wa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu. Wanafurahi mchana kutwa kwa sababu yako, na kukusifu kwa ajili ya uadilifu wako. Wewe ndiwe fahari na nguvu yao; kwa wema wako twapata ushindi. Ee Mwenyezi-Mungu, mlinzi wetu ni wako, mfalme wetu ametoka kwako ewe Mtakatifu wa Israeli. Zamani ulinena katika maono, ukawaambia watumishi wako waaminifu: “Nimempa nguvu shujaa mmoja, nimemkuza huyo niliyemteua kati ya watu. Nimempata Daudi, mtumishi wangu; nimemweka wakfu kwa mafuta yangu matakatifu. Mkono wangu wa nguvu utakuwa naye daima; mkono wangu mimi mwenyewe utamwimarisha. Maadui hawataweza kumshinda, wala waovu hawatamnyanyasa. Mimi nitawaponda wapinzani wake; nitawaangamiza wote wanaomchukia. Nitakuwa mwaminifu kwake na kumfadhili, kwa jina langu atapata ushindi mkubwa. Nitaimarisha nguvu na utawala wake, toka bahari hata mito. Yeye ataniita: ‘Wewe ni Baba yangu, Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu.’ Nami nitamfanya kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, mkuu kuliko wafalme wote duniani. Fadhili zangu nitamwekea milele, na agano langu kwake litadumu daima. Nitaudumisha daima ukoo wake wa kifalme, na ufalme wake kama mbingu. “Lakini wazawa wake wakiiacha sheria yangu, wasipoishi kadiri ya maagizo yangu, kama wakizivunja kanuni zangu, na kuacha kutii amri zangu, hapo nitawaadhibu makosa yao; nitawapiga kwa sababu ya uovu wao. Lakini sitaacha kumfadhili Daudi, wala kuwa mwongo kuhusu uaminifu wangu. Sitavunja agano langu naye, wala kubatili neno nililotamka kwa mdomo wangu. “Nimeapa mara moja tu kwa utakatifu wangu; nami sitamwambia Daudi uongo. Ukoo wake utadumu milele; na ufalme wake kama jua. Utadumu milele kama mwezi utokezavyo angani.” Lakini sasa ee Mungu, umemtupa na kumkataa, umejaa ghadhabu dhidi ya huyo uliyemweka wakfu. Umefuta agano ulilofanya na mtumishi wako; umeitupa taji yake mavumbini. Kuta zote za mji wake umezibomoa; ngome zake umezivunjavunja. Wote wapitao wanampokonya mali zake; amekuwa dharau kwa jirani zake. Maadui zake umewapa ushindi; umewafurahisha maadui zake wote. Silaha zake umezifanya butu; ukamwacha ashindwe vitani. Umemvua madaraka yake ya kifalme ukauangusha chini utawala wake. Umezipunguza siku za ujana wake, ukamfunika fedheha tele. Ee Mwenyezi-Mungu, utajificha hata milele? Hata lini hasira yako itawaka kama moto? Ukumbuke, ee Bwana, ufupi wa maisha yangu; kwamba binadamu uliyemuumba anaishi muda mfupi! Ni mtu gani aishiye asipate kufa? Nani awezaye kujiepusha na kifo? Ee Bwana, ziko wapi basi fadhili zako, ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako? Ee Bwana, ukumbuke anavyotukanwa mtumishi wako, jinsi nivumiliavyo matusi ya wasiokujua. Ona wanavyomzomea, ee Mwenyezi-Mungu; jinsi wanavyomdhihaki mteule wako kila aendako. Asifiwe Mwenyezi-Mungu milele! Amina! Amina! (Sala ya Mose, mtu wa Mungu) Ee Bwana, tangu vizazi vyote, wewe umekuwa usalama wetu. Kabla ya kuwapo milima, kabla hujauumba ulimwengu; wewe ndiwe Mungu, milele na milele. Wamwambia binadamu, “Rudi mavumbini!” Naye binadamu hurudi mavumbini alimotoka! Kwako miaka elfu ni kama siku moja tu, ni kama jana ambayo imekwisha pita; kwako ni kama mkesha mmoja wa usiku! Wawafutilia mbali watu kama ndoto! Binadamu ni kama nyasi zinazochipua asubuhi: Asubuhi huchipua na kuchanua, jioni zimekwisha nyauka na kukauka. Hasira yako inatuangamiza; tunatishwa na ghadhabu yako. Maovu yetu umeyaweka mbele yako; dhambi zetu za siri ziko wazi mbele yako. Kwa hasira yako maisha yetu yatoweka, yanaisha kama pumzi. Miaka ya kuishi ni sabini, au tukiwa wenye afya, themanini; lakini yote ni shida na taabu! Siku zapita mbio, nasi twatoweka mara! Nani anayetambua uzito wa hasira yako? Nani anayejali matokeo ya ghadhabu yako? Utufundishe ufupi wa maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima. Urudi, ee Mwenyezi-Mungu! Utakasirika hata lini? Utuonee huruma sisi watumishi wako. Utushibishe fadhili zako asubuhi, tushangilie na kufurahi maisha yetu yote. Utujalie sasa miaka mingi ya furaha, kama ulivyotupa miaka mingi ya shida na taabu. Utuoneshe matendo yako sisi watumishi wako; uwaoneshe wazawa wetu uwezo wako mtukufu. Utufadhili ee Bwana, Mungu wetu; uzitegemeze kazi zetu, uzifanikishe shughuli zetu. Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!” Hakika Mungu atakuokoa katika mtego; atakukinga na maradhi mabaya. Atakufunika kwa mabawa yake, utapata usalama kwake; mkono wake utakulinda na kukukinga. Huna haja ya kuogopa vitisho vya usiku, wala shambulio la ghafla mchana; huna haja ya kuogopa baa lizukalo usiku, wala maafa yanayotokea mchana. Hata watu elfu wakianguka karibu nawe, naam, elfu kumi kuliani mwako, lakini wewe baa halitakukaribia. Kwa macho yako mwenyewe utaangalia, na kuona jinsi watu waovu wanavyoadhibiwa. Wewe umemfanya Mwenyezi-Mungu kuwa kimbilio lako; naam, Mungu aliye juu kuwa kinga yako. Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.” (Zaburi. Wimbo wa siku ya Sabato) Ni vema kukushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kuliimbia sifa jina lako, ee Mungu Mkuu. Ni vema kutangaza fadhili zako asubuhi, na uaminifu wako nyakati za usiku, kwa muziki wa zeze na kinubi, kwa sauti tamu ya zeze. Ee Mwenyezi-Mungu, matendo yako yanifurahisha; nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda. Matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, ni makuu mno! Mawazo yako ni mazito mno! Mtu mpumbavu hawezi kufahamu, wala mjinga hajui jambo hili: Kwamba waovu waweza kustawi kama nyasi, watenda maovu wote waweza kufanikiwa, lakini mwisho wao ni kuangamia milele, bali wewe, ee Mwenyezi-Mungu, u mkuu milele. Hao maadui zako, ee Mwenyezi-Mungu, naam, hao maadui zako, hakika wataangamia; wote watendao maovu, watatawanyika! Wewe umenipa nguvu kama nyati; umenimiminia mafuta ya kuburudisha. Kwa macho nimeona maadui zangu wameshindwa; nimesikia kilio chao watendao maovu. Waadilifu hustawi kama mitende; hukua kama mierezi ya Lebanoni! Kama miti iliyopandwa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu, hustawi katika nyua za Mungu wetu; huendelea kuzaa matunda hata uzeeni; daima wamejaa utomvu na wabichi; wapate kutangaza kwamba Mwenyezi-Mungu ni mnyofu, Mwamba wangu, kwake hamna upotovu. Mwenyezi-Mungu anatawala; amejivika fahari kuu! Mwenyezi-Mungu amevaa fahari na nguvu! Ameuimarisha ulimwengu, nao hautatikisika kamwe. Kiti chako cha enzi ni imara tangu kale; wewe umekuwapo kabla ya nyakati zote. Vilindi vimetoa sauti, ee Mwenyezi-Mungu; naam, vimepaza sauti yake, vilindi vyapaza tena mvumo wake. Mwenyezi-Mungu ana enzi kuu juu mbinguni, ana nguvu kuliko mlio wa bahari, ana nguvu kuliko mawimbi ya maji. Ee Mwenyezi-Mungu, maagizo yako ni thabiti; nyumba yako ni takatifu milele na milele. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu mwenye kulipiza kisasi, ewe Mungu mlipiza kisasi, ujitokeze! Usimame, ee hakimu wa watu wote; uwaadhibu wenye kiburi wanavyostahili! Waovu wataona fahari hata lini? Watajisifia mpaka lini, ee Mwenyezi-Mungu? Hata lini waovu watajigamba kwa maneno? Waovu wote watajivuna mpaka lini? Wanawaangamiza watu wako, ee Mwenyezi-Mungu, wanawakandamiza hao walio mali yako. Wanawaua wajane na wageni; wanawachinja yatima! Wanasema: “Mwenyezi-Mungu haoni, Mungu wa Yakobo hajui!” Enyi wajinga wa mwisho, fikirini kidogo! Enyi wapumbavu, mtapata lini maarifa? Aliyefanya sikio, je, hawezi kusikia? Aliyeumba jicho, je, hawezi kuona? Mwenye kutawala mataifa, je, hawezi kuadhibu? Mkufunzi wa wanadamu, je, hana maarifa? Mwenyezi-Mungu ayajua mawazo ya watu; anajua kwamba hayafai kitu. Heri mtu unayemfunza nidhamu, ee Mwenyezi-Mungu, mtu unayemfundisha sheria yako, ili siku ya taabu apate utulivu, hadi waovu wachimbiwe shimo. Mwenyezi-Mungu hatawaacha watu wake; hatawatupa hao walio mali yake. Maana hukumu zitatolewa kwa haki tena, na wanyofu wote wa moyo wataizingatia. Nani aliyenisaidia kumpinga mtu mwovu? Nani aliyekuwa upande wangu dhidi ya wabaya? Mwenyezi-Mungu asingalinisaidia, ningalikwisha kwenda kwenye nchi ya wafu. Nilipohisi kwamba ninateleza, fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, zilinitegemeza. Mahangaiko ya moyo wangu yanapozidi, wewe wanifariji na kunifurahisha. Wewe huwezi kushirikiana na mahakimu dhalimu, wanaotunga kanuni za kutetea maovu. Wao wanaafikiana kuwaangamiza waadilifu, na kuwahukumu watu wasio na hatia wauawe. Lakini Mwenyezi-Mungu ni ngome yangu; Mungu wangu ni mwamba wa usalama wangu. Uovu wao atawarudishia wao wenyewe, atawafutilia mbali kwa sababu ya ubaya wao. Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, atawafutilia mbali! Njoni tumwimbie Mwenyezi-Mungu, tumshangilie mwamba wa wokovu wetu! Twende mbele zake na shukrani; tumshangilie kwa nyimbo za sifa. Maana Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mkuu; yeye ni Mfalme mkuu juu ya miungu yote. Vilindi vyote vya dunia vimo mikononi mwake, vilele vya milima ni vyake. Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya; kwa mikono yake aliiumba nchi kavu. Njoni tusujudu na kumwabudu; tumpigie magoti Mwenyezi-Mungu, Muumba wetu! Maana yeye ni Mungu wetu, nasi ni watu wa kundi lake, ni kondoo wake anaowachunga. Laiti leo mngesikiliza sauti yake: “Msiwe wakaidi kama kule Meriba, kama walivyokuwa kule Masa jangwani, wazee wenu waliponijaribu na kunipima, ingawa walikuwa wameona mambo niliyowatendea. Kwa miaka arubaini nilichukizwa nao, nikasema: ‘Kweli, hawa ni watu waliopotoka! Hawajali kabisa njia zangu!’ Basi, nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko!’” Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu na kulisifu jina lake. Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu. Yatangazieni mataifa utukufu wake, waambieni watu wote matendo yake ya ajabu. Maana Mwenyezi-Mungu ni mkuu, anasifika sana; anastahili kuheshimiwa kuliko miungu yote. Miungu ya mataifa mengine si kitu; lakini Mwenyezi-Mungu aliziumba mbingu. Utukufu na fahari vyamzunguka; nguvu na uzuri vyalijaza hekalu lake. Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima, enyi jamii zote za watu; naam, kirini utukufu na nguvu yake. Lisifuni jina lake tukufu; leteni tambiko na kuingia hekaluni mwake. Mwabuduni Mwenyezi-Mungu katika patakatifu pake; tetemekeni mbele yake ee dunia yote! Yaambieni mataifa: “Mwenyezi-Mungu anatawala! Ameuweka ulimwengu imara, hautatikisika. Atawahukumu watu kwa haki!” Furahini enyi mbingu na dunia! Bahari na ivume pamoja na vyote vilivyomo! Furahini enyi mashamba na vyote vilivyomo! Ndipo miti yote misituni itaimba kwa furaha, mbele ya Mwenyezi-Mungu anayekuja; naam, anayekuja kuihukumu dunia. Ataihukumu dunia kwa haki, na mataifa kwa uaminifu wake. Mwenyezi-Mungu anatawala! Furahi, ee dunia! Furahini enyi visiwa vingi! Mawingu na giza nene vyamzunguka; uadilifu na haki ni msingi wa utawala wake. Moto watangulia mbele yake, na kuwateketeza maadui zake pande zote. Umeme wake wauangaza ulimwengu; dunia yauona na kutetemeka. Milima yayeyuka kama nta mbele ya Mwenyezi-Mungu; naam, mbele ya Bwana wa dunia yote. Mbingu zatangaza uadilifu wake; na mataifa yote yauona utukufu wake. Wote wanaoabudu sanamu wanaaibishwa, naam, wote wanaojisifia miungu duni; miungu yote husujudu mbele zake. Watu wa Siyoni wanafurahi; watu wa Yuda wanashangilia, kwa sababu ya hukumu zako, ee Mungu. Wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu juu ya dunia yote; wewe watukuka juu ya miungu yote. Mwenyezi-Mungu huwapenda wanaochukia uovu, huyalinda maisha ya watu wake; huwaokoa makuchani mwa waovu. Mwanga humwangazia mtu mwadilifu, na furaha kwa watu wanyofu wa moyo. Furahini kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu; mshukuruni kwa ajili ya jina lake takatifu. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu! Mkono wake hodari, mkono wake mtakatifu umempatia ushindi. Mwenyezi-Mungu ameonesha ushindi wake; ameyadhihirishia mataifa uwezo wake wa kuokoa. Amekumbuka fadhili na uaminifu wake kwa Waisraeli. Pande zote za dunia zimeuona ushindi wa Mungu wetu. Dunia yote imshangilie Mwenyezi-Mungu; imsifu kwa nyimbo na vigelegele. Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa shangwe, msifuni kwa sauti tamu za zeze. Mpigieni vigelegele Mwenyezi-Mungu mfalme wetu, mshangilieni kwa tarumbeta na sauti ya baragumu. Bahari na ivume na vyote vilivyomo; dunia na wote waishio ndani yake. Enyi mito pigeni makofi; enyi vilima imbeni pamoja kwa shangwe. Shangilieni mbele ya Mwenyezi-Mungu, maana anakuja kutawala dunia. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, atawatawala watu kwa uadilifu. Mwenyezi-Mungu anatawala, mataifa yanatetemeka! Ameketi juu ya viumbe vyenye mabawa, nayo dunia inatikisika! Mwenyezi-Mungu ni mkuu katika Siyoni; ametukuka juu ya mataifa yote. Wote na walisifu jina lake kuu la kutisha. Mtakatifu ndiye yeye! Ee mfalme mkuu, mpenda uadilifu! Umethibitisha haki katika Israeli; umeleta uadilifu na haki. Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; angukeni kifudifudi mbele zake. Mtakatifu ndiye yeye! Mose na Aroni walikuwa makuhani wake; Samueli alikuwa miongoni mwa waliomlilia. Walimlilia Mwenyezi-Mungu naye akawasikiliza. Alisema nao katika mnara wa wingu; waliyazingatia matakwa yake na amri alizowapa. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wewe uliwasikiliza; kwao ulikuwa Mungu mwenye kusamehe, ingawa uliwaadhibu kwa makosa yao. Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; abuduni katika mlima wake mtakatifu! Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ni mtakatifu. (Zaburi ya shukrani) Mshangilieni Mwenyezi-Mungu, enyi nchi zote! Mwabuduni Mwenyezi-Mungu kwa furaha, nendeni kwake mkiimba kwa shangwe! Jueni kwamba Mwenyezi-Mungu ni Mungu. Yeye ndiye aliyetuumba, nasi ni mali yake; sisi ni watu wake, ni kondoo wa malisho yake. Pitieni milango ya hekalu lake kwa shukrani, ingieni katika nyua zake kwa sifa. Mshukuruni na kulisifu jina lake. Mwenyezi-Mungu ni mwema; fadhili zake zadumu milele, na uaminifu wake katika vizazi vyote. (Zaburi ya Daudi) Utenzi wangu kuhusu uaminifu na haki; ninauimba kwa heshima yako, ee Mwenyezi-Mungu. Nitazingatia mwenendo usio na hatia. Je, utakuja kwangu lini? Nitaishi kwa unyofu nyumbani kwangu; sitavumilia kamwe upuuzi. Nayachukia matendo ya watu wapotovu, mambo yao hayataambatana nami. Upotovu wowote ule uwe mbali nami; sitahusika kabisa na uovu. Anayemsengenya jirani nitamfutilia mbali; sitamvumilia mwenye majivuno na kiburi. Nitawaangalia kwa wema watu walio waaminifu, wapate kuishi pamoja nami. Watu wanyofu ndio watakaonitumikia. Mwongo yeyote hatakaa nyumbani mwangu; hakuna msema uongo atakayekaa kwangu. Siku kwa siku nitawaangamiza waovu wote nchini; nitawaangamiza wabaya wote mjini mwa Mwenyezi-Mungu. (Sala ya mtu aliye katika shida na ambaye anamwekea Mwenyezi-Mungu malalamiko yake) Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu, na kilio changu kikufikie. Usijifiche mbali nami wakati wa taabu! Unitegee sikio lako, unijibu upesi wakati ninapokuomba! Siku zangu zapita kama moshi; mifupa yangu yaungua kama katika tanuri. Nimepondwa moyoni kama nyasi na kunyauka; sina hata hamu ya chakula. Kutokana na kusononeka kwangu, nimebaki mifupa na ngozi. Nimekuwa kama ndege wa jangwani; kama bundi kwenye mahame. Ninalala macho wazi, kama ndege mkiwa juu ya paa. Mchana kutwa maadui zangu wananisimanga, wanaonidhihaki hutumia jina langu kulaania. Majivu yamekuwa chakula changu, machozi nayachanganya na kinywaji changu, kwa sababu ya ghadhabu na hasira yako, maana umeniokota na kunitupilia mbali. Maisha yangu ni kama kivuli cha jioni; ninanyauka kama nyasi. Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, watawala milele; jina lako lakumbukwa vizazi vyote. Wewe utainuka na kuurehemu mji wa Siyoni; maana wakati umefika wa kuutendea mema; wakati wake uliopangwa umefika. Watumishi wako wanauthamini sana, ujapokuwa magofu sasa; wanauonea huruma, ingawa umeharibika kabisa. Mataifa yataliheshimu jina la Mwenyezi-Mungu; wafalme wote duniani wataogopa utukufu wake. Mwenyezi-Mungu ataijenga upya Siyoni, na kuonekana alivyo mtukufu. Ataikubali sala ya fukara; wala hatayakataa maombi yao. Andika jambo hili kwa ajili ya vizazi vijavyo; watakaozaliwa baadaye wamsifu Mwenyezi-Mungu. Kwamba aliangalia chini kutoka patakatifu pake juu, Mwenyezi-Mungu aliangalia dunia kutoka mbinguni, akasikia lalamiko la wafungwa; akawaachilia huru waliohukumiwa kuuawa. Hivyo watu watatangaza jina la Mwenyezi-Mungu huko Siyoni; sifa zake zitatangazwa huko Yerusalemu, wakati mataifa yatakapokusanyika pamoja na falme zitakutana kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Mungu amenipunguzia nguvu ningali kijana; ameyafupisha maisha yangu. Ee Mungu wangu, usinichukue sasa wakati ningali bado kijana. Ee Mwenyezi-Mungu wewe wadumu milele. Wewe uliiumba dunia zamani za kale, mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki; hizo zitachakaa kama vazi. Utazitupilia mbali kama nguo, nazo zitapotelea mbali. Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayana mwisho. Watoto wa watumishi wako watakaa salama; wazawa wao wataimarishwa mbele yako. (Zaburi ya Daudi) Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu; nafsi yangu yote ilisifu jina lake takatifu! Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu! Usisahau kamwe wema wake wote. Ndiye anayenisamehe uovu wangu wote, na kuniponya magonjwa yote. Ndiye aniokoaye kutoka kifoni, na kunijalia rehema na fadhili zake. Ndiye anayeniridhisha mema maisha yangu yote, hata nabaki kijana mwenye nguvu kama tai. Mwenyezi-Mungu huhukumu kwa haki; huwajalia wanaodhulumiwa haki zao. Alimjulisha Mose mwongozo wake, aliwaonesha watu wa Israeli matendo yake. Mwenyezi-Mungu ni mwenye rehema na huruma; ni mvumilivu na mwingi wa fadhili. Hatukemeikemei daima, wala hasira yake haidumu milele. Yeye hatuadhibu kama tunavyostahili; hatulipizi kadiri ya uovu wetu. Kama vile anga lilivyo juu mbali na dunia, ndivyo ulivyo mwingi wema wake kwa watu wanaomcha. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo azitengavyo dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba amhurumiavyo mwanawe, ndivyo Mwenyezi-Mungu awahurumiavyo wote wamchao. Mungu ajua mfumo wa nafsi zetu; ajua kwamba sisi ni mavumbi. Walakini binadamu, maisha yake ni kama nyasi tu; huchanua kama ua shambani: Upepo huvuma juu yake nalo latoweka; na mahali lilipokuwa hapaonekani tena. Lakini fadhili za Mwenyezi-Mungu hudumu milele, kwa wale wote wanaomheshimu; na wema wake wadumu vizazi vyote, kwa wote wanaozingatia agano lake, wanaokumbuka kutii amri zake. Mwenyezi-Mungu ameweka kiti chake cha enzi mbinguni; yeye anatawala juu ya vitu vyote. Enyi malaika wakuu, msifuni Mwenyezi-Mungu; mnaotimiza amri zake na kutekeleza neno lake! Enyi jeshi lote la mbinguni, msifuni Mwenyezi-Mungu; enyi watumishi wake mnaotekeleza matakwa yake! Msifuni Mwenyezi-Mungu enyi viumbe vyake vyote; msifuni popote mlipo katika milki yake. Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu! Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu! Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, wewe ni mkuu mno! Umejivika utukufu na fahari. Umejizungushia mwanga kama vazi, umezitandaza mbingu kama hema; umejenga makao yako juu ya maji ya mbingu. Umeyafanya mawingu kuwa gari lako; waruka juu ya mabawa ya upepo, waufanya upepo kuwa mjumbe wako, moto na miali yake kuwa watumishi wako. Dunia umeiweka imara juu ya misingi yake, ili isitikisike milele. Uliifunika dunia kwa bahari kama vazi, na maji yakaimeza milima mirefu. Ulipoyakaripia, maji yalikimbia, yaliposikia ngurumo yako yalitimka mbio. Yaliporomoka toka milimani hadi mabondeni, mpaka pale mahali ulipoyatengenezea. Uliyawekea hayo maji mipaka, yasije yakaifunika tena dunia. Umetokeza chemchemi mabondeni, na mikondo yake ipite kati ya vilima. Hizo zawapatia maji wanyama wote porini. Humo pundamwitu huzima kiu zao. Ndege hujenga viota vyao katika miti ya hapo, hutua katika matawi yake na kuimba. Toka juu angani wainyeshea milima mvua, nayo dunia waitosheleza kwa baraka yako. Waotesha nyasi kwa ajili ya mifugo, na mimea kwa matumizi ya binadamu ili naye ajipatie chakula chake ardhini: Divai ya kumchangamsha, mafuta ya zeituni ya kumfurahisha, na mkate wa kumpa nguvu. Miti mikubwa ya Mwenyezi-Mungu yapata maji ya kutosha; naam, mierezi ya Lebanoni aliyoiotesha. Humo, ndege hujenga viota vyao; korongo hufanya maskani yao katika misonobari. Milima mirefu ni makao ya mbuzimwitu; na pelele hupata maficho yao miambani. Umeuumba mwezi utupimie majira; jua nalo lajua wakati wa kutua. Waleta giza, usiku waingia; nao wanyama wote wa porini wanatoka: Wanasimba hunguruma wapate mawindo, humngojea Mungu awape chakula chao. Jua lichomozapo hurudi makwao, na kujipumzisha mapangoni mwao. Hapo naye binadamu huenda kwenye shughuli zake; na kufanya kazi zake mpaka jioni. Ee Mwenyezi-Mungu, umetenda mambo mengi mno! Yote umeyafanya kwa hekima! Dunia imejaa viumbe vyako! Mbali kule iko bahari - kubwa na pana, ambamo kumejaa viumbe visivyohesabika, viumbe hai, vikubwa na vidogo. Ndimo zinamosafiri meli, na lile dude Lewiyathani uliloliumba licheze humo. Wote wanakungojea wewe, uwapatie chakula chao kwa wakati wake. Wanaokota chochote kile unachowapa; ukifumbua mkono wako wanashiba vinono. Ukiwapa kisogo, wanaogopa; ukiondoa pumzi yao, wanakufa, na kurudi mavumbini walimotoka. Ukiwapulizia pumzi yako, wanaishi tena; wewe waipa dunia sura mpya. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu udumu milele; Mwenyezi-Mungu apendezwe na matendo yake mwenyewe. Huitazama dunia nayo hutetemeka, huigusa milima nayo hutoa moshi! Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote; nitamsifu Mungu wangu muda wote niishipo. Upendezwe, ee Mwenyezi-Mungu, na mawazo yangu haya; maana furaha yangu naipata kwako. Wenye dhambi waondolewe duniani, pasiwe na waovu wowote tena! Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, tangazeni ukuu wake; yajulisheni mataifa mambo aliyotenda! Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa; simulieni matendo yake ya ajabu! Jisifieni jina lake takatifu; wenye kumcha Mwenyezi-Mungu na wafurahi. Tafuteni msaada kwa Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu; mwendeeni Mwenyezi-Mungu daima. Kumbukeni matendo ya ajabu aliyotenda, miujiza yake na hukumu alizotoa, enyi wazawa wa Abrahamu mtumishi wake, enyi wazawa wa Yakobo, wateule wake; Yeye ndiye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; hukumu zake zina nguvu duniani kote. Yeye hulishika agano lake milele, hutimiza ahadi zake kwa vizazi elfu. Hushika agano alilofanya na Abrahamu, na ahadi aliyomwapia Isaka. Alimthibitishia Yakobo ahadi yake, alimhakikishia Israeli agano hilo la milele. Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani, nayo itakuwa mali yenu wenyewe.” Watu wa Mungu walikuwa wachache; hawakuwa maarufu, tena walikuwa wageni nchini Kanaani. Walitangatanga kutoka taifa hadi taifa; kutoka nchi moja hadi nchi nyingine. Lakini Mungu hakuruhusu mtu awadhulumu; kwa ajili yao aliwaonya wafalme: “Msiwaguse wateule wangu; msiwadhuru manabii wangu!” Mungu alizusha njaa nchini mwao, akaharibu chakula chao chote. Lakini aliwatangulizia mtu mmoja, Yosefu aliyekuwa ameuzwa utumwani. Walimfunga miguu kwa minyororo, na shingoni kwa nira ya chuma, Muda si muda alichotabiri kilitimia. neno la Mwenyezi-Mungu lilimdhibiti. Mfalme wa Misri akaamuru afunguliwe; mtawala wa mataifa akamwachilia huru. Alimweka kuwa mkurugenzi wa serikali yake, na mkuu wa mali yake yote; awaongoze maofisa wake apendavyo, na kuwafundisha wazee wake hekima. Ndipo Israeli akaingia nchini Misri; Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu. Mwenyezi-Mungu akawafanya watu wake wazae sana; akawajalia nguvu kuliko maadui zao. Aliwafanya Wamisri wawachukie watu wake, wakawatendea hila watumishi wake. Kisha akamtuma Mose mtumishi wake, akamtuma na Aroni mteule wake. Wakafanya ishara za Mungu kati ya Wamisri, na miujiza katika nchi hiyo ya Hamu. Mungu akaleta giza juu ya nchi; lakini Wamisri wakakataa kutii amri zake. Akageuza mito yao kuwa damu, akawaua samaki wao wote. Vyura wakaivamia nchi yao, hata jumba la mfalme likajawa nao. Mungu akanena, kukazuka makundi ya nzi, na viroboto katika nchi yote. Badala ya mvua akawapa mvua ya mawe, na umeme uliomulika nchi yao yote; akaharibu mizabibu na mitini yao, akaivunja pia miti ya nchi yao. Mungu akanena, kukazuka nzige, na panzi maelfu yasiyohesabika; wakaitafuna mimea yote katika nchi, wakayala mazao yao yote. Aliwaua wazaliwa wa kwanza nchini mwao, chipukizi wa kwanza wa jamaa za Wamisri. Kisha akawatoa watu wa Israeli nchini, wakiwa na fedha na dhahabu; wala hakuna hata mmoja wao aliyejikwaa. Wamisri walifurahia kuondoka kwao, kwani hofu iliwashika kwa sababu yao. Mungu alitandaza wingu juu ya watu wake, na moto ili kuwaangazia usiku. Waliomba naye akawaletea kware, akawapa mkate kutoka mbinguni kwa wingi. Alipasua mwamba maji yakabubujika; yakatiririka jangwani kama mto. Aliikumbuka ahadi yake takatifu, aliyompa Abrahamu mtumishi wake. Basi akawatoa watu wake nchini, wateule wake wakaimba na kushangilia. Aliwapa nchi za mataifa mengine na kuwakabidhi mashamba ya wenyeji; kusudi watu wake watii masharti yake, na kufuata sheria zake. Asifiwe Mwenyezi-Mungu! Haleluya! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele! Ni nani awezaye kutaja matendo ya Mwenyezi-Mungu? Ni nani awezaye kumsifu kama anavyostahili? Heri wale wanaotekeleza haki, wanaotenda daima mambo yaliyo sawa. Unikumbuke ee Mwenyezi-Mungu unapowafadhili watu wako; unisaidie wakati unapowaokoa; ili niweze kuona fanaka ya wateule wako, nipate kufurahia furaha ya taifa lako, na kuona fahari pamoja na watu wako. Tumetenda dhambi sisi na wazee wetu; tumetenda maovu, tumefanya mabaya. Wazee wetu walipokuwa Misri, hawakujali matendo ya ajabu ya Mungu; hawakukumbuka wingi wa fadhili zake, bali walimwasi kando ya bahari ya Shamu. Hata hivyo Mungu aliwaokoa kama alivyoahidi, ili aoneshe nguvu yake kuu. Aliikemea bahari ya Shamu ikakauka; akawapitisha humo kama katika nchi kavu. Aliwaokoa mikononi mwa waliowachukia; aliwaokoa kutoka kwa nguvu za maadui zao. Maji ya bahari yaliwafunika maadui zao; wala hakusalia hata mmoja wao. Hapo watu wake wakaamini maneno yake, wakamwimbia tenzi za sifa yake. Lakini mara walisahau matendo yake, wakaacha kutegemea shauri lake. Walijawa na tamaa kubwa kule jangwani, wakamjaribu Mungu kule nyikani. Naye akawapa kile walichoomba, lakini akapeleka maradhi mabaya kati yao. Kule kambini walimwonea wivu Mose, na Aroni mtumishi mtakatifu wa Mwenyezi-Mungu. Ndipo ardhi ikafunguka ikammeza Dathani, na kumzika Abiramu na kundi lake lote; moto ukawatokea wafuasi wao, ukawateketeza watu hao waovu. Walitengeneza ndama wa dhahabu kule Horebu, wakaiabudu sanamu hiyo ya kusubu; waliubadilisha utukufu wa Mungu, kwa sanamu ya mnyama ambaye hula nyasi. Walimsahau Mungu aliyewaokoa, aliyetenda mambo makuu nchini Misri, maajabu katika nchi hiyo ya Hamu, na mambo ya kutisha katika bahari ya Shamu. Mungu alisema atawaangamiza watu wake, ila tu Mose mteule wake aliingilia kati, akaizuia hasira yake isiwaangamize. Kisha wakaidharau nchi ile ya kupendeza, kwa sababu hawakuwa na imani na ahadi ya Mungu. Walinungunika mahemani mwao, wala hawakumsikiliza Mwenyezi-Mungu. Hivyo Mungu akainua mkono akaapa kwamba atawaangamizia jangwani; atawatawanya wazawa wao kati ya watu, na kuwasambaza duniani kote. Kisha wakajiunga kumwabudu Baali kule Peori, wakala tambiko zilizotambikiwa mizimu. Waliichochea hasira ya Mwenyezi-Mungu kwa matendo yao, maradhi mabaya yakazuka kati yao. Lakini Finehasi akasimama kufanya malipizi, na yale maradhi yakakoma. Jambo hilo lakumbukwa kwa heshima yake, tangu wakati huo na nyakati zote. Walimkasirisha Mungu penye maji ya Meriba, Mose akapata taabu kwa ajili yao. Walimtia Mose uchungu rohoni, hata akasema maneno bila kufikiri. Hawakuwaua watu wa mataifa mengine kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Bali walijumuika na watu wa mataifa, wakajifunza kutenda mambo yao. Waliabudu sanamu za miungu yao, nazo zikawa mtego wa kuwaangamiza. Waliwaua watoto wao wa kiume na wa kike, wakawatoa tambiko kwa pepo. Walimwaga damu ya wasio na hatia, damu ya watoto wao wa kiume na wa kike ambao waliwatoa tambiko kwa sanamu za Kanaani, nayo nchi ikatiwa unajisi kwa mauaji hayo. Hivyo wakafanywa najisi kwa matendo yao, 2wakakosa uaminifu kwa Mungu kama wazinzi. Hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawawakia watu wake, akachukizwa sana na hao waliokuwa mali yake. Akawatia makuchani mwa watu wa mataifa, hao wenye kuwachukia wakawatawala. Maadui zao waliwakandamiza, wakawatumikisha kwa nguvu. Mara nyingi Mungu aliwaokoa watu wake, lakini wao wakachagua kumwasi, wakazidi kuzama katika uovu wao. Hata hivyo Mungu alizijali taabu zao, wakati aliposikia kilio chao; kwa ajili yao alilikumbuka agano lake, akawahurumia kwa wingi wa fadhili zake. Aliwafanya waliowakandamiza wawaonee huruma. Utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, utukusanye pamoja kutoka kwa mataifa, tupate kulisifu jina lako takatifu, na kuona fahari juu ya sifa zako. Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele! Na watu wote waseme: “Amina!” Asifiwe Mwenyezi-Mungu! Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele! Semeni hivyo, enyi mliokombolewa na Mwenyezi-Mungu, watu ambao aliwaokoa katika taabu, akawakusanyeni kutoka nchi za kigeni: Kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini. Baadhi walitangatanga katika jangwa tupu, wasiweze kufikia mji wa kukaa. Waliona njaa na kiu; wakavunjika moyo kabisa. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwaongoza katika njia iliyonyoka, mpaka wakaufikia mji wa kukaa. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huwatosheleza walio na kiu; na wenye njaa huwashibisha mema. Baadhi waliishi katika giza na ukiwa, wafungwa katika mateso na minyororo, kwa sababu waliasi maagizo ya Mungu, na kuyapuuza mashauri yake Mungu Mkuu. Walikuwa hoi kwa kazi ngumu, wakaanguka chini, pasiwe na wa kuwasaidia. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwatoa katika giza na ukiwa, na minyororo yao akaivunjavunja. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huvunja na kufungua milango ya shaba, na kukatakata fito za chuma. Baadhi walipumbaa kwa sababu ya dhambi zao, waliteseka kwa sababu ya uovu wao; chakula kikawa kinyaa kwao, wakawa nusura wafe. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Kwa neno lake aliwaponya, akawaokoa wasiangamie. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Wamtolee tambiko za shukrani; wasimulie matendo yake kwa nyimbo za shangwe. Baadhi walisafiri baharini kwa meli, na kufanya shughuli zao humo baharini. Waliyaona matendo ya Mwenyezi-Mungu, mambo ya ajabu aliyotenda huko. Aliamuru, akazusha dhoruba kali, ikarusha juu mawimbi ya bahari. Walitupwa juu angani, kisha chini vilindini; uhodari wao ukawaishia katika mkasa huo. Waliyumbayumba na kupepesuka kama walevi; maarifa yao ya uanamaji yakawaishia. Ndipo katika taabu zao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso zao. Aliifanya ile dhoruba kali itulie, nayo mawimbi yakanyamaza. Hapo wakafurahi kwa kupata utulivu; akawafikisha kwenye bandari waliyoiendea. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Mtukuzeni katika kusanyiko la watu, na kumsifu katika baraza la wazee. Mungu aliigeuza mito kuwa jangwa, chemchemi akazikausha kabisa. Ardhi yenye rutuba akaifanya udongo wa chumvi, kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Aligeuza majangwa kuwa mabwawa ya maji, na nchi kame kuwa chemchemi za maji. Akawahamishia huko wenye njaa, nao wakajenga mji wa kukalika. Walilima mashamba na kupanda mizabibu, wakavuna mazao kwa wingi. Aliwabariki watu wake, wakaongezeka; na idadi ya wanyama wao akaizidisha. Kisha walipopungua na kuwa wanyonge, kwa kukandamizwa, kuteswa na huzuni, aliwadharau wakuu waliowatesa, akawazungusha jangwani kusiko na njia. Lakini aliwaokoa wahitaji katika taabu zao, akaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo. Waadilifu waonapo jambo hilo wanafurahi, lakini waovu wote wananyamazishwa. Wenye hekima na wayafikirie mambo haya, wazitambue fadhili zake Mwenyezi-Mungu. (Zaburi ya Daudi: Wimbo) Niko thabiti moyoni, ee Mungu, naam, niko thabiti moyoni; nitaimba na kukushangilia! Amka, ee nafsi yangu! Amkeni enyi kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko! Ee Mwenyezi-Mungu, nitakushukuru kati ya mataifa; nitakuimbia sifa kati ya mataifa. Fadhili zako ni kubwa kuliko mbingu; uaminifu wako waenea hata mawinguni. Utukuzwe, ee Mungu juu ya mbingu! Utukufu wako uenee duniani kote! Watu hao uwapendao na wasalimishwe; utusaidie kwa mkono wako na kutusikiliza. Mungu amesema kutoka patakatifu pake: “Sasa nitaigawa Shekemu kwa shangwe, bonde la Sukothi nitalipima sehemusehemu. Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu; Efraimu ni kofia yangu ya chuma, na Yuda ni fimbo yangu ya enzi. Moabu ni kama bakuli langu la kunawia; kiatu changu nitaitupia Edomu kuimiliki. Nitapiga kelele ya ushindi juu ya Filistia!” Ni nani, atakayenipeleka kwenye mji wa ngome? Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu? Je, umetuacha kabisa, ee Mungu? Wewe huendi tena na majeshi yetu! Utupatie msaada dhidi ya maadui zetu, maana msaada wa binadamu haufai kitu. Mungu akiwa upande wetu tutashinda, yeye atawaponda maadui zetu. (Kwa Mwimbishaji. Wimbo wa Daudi) Usinyamaze, ee Mungu ninayekusifu! Watu waovu na wadanganyifu wanishambulia, wanasema uongo dhidi yangu. Wanasema maovu juu yangu, na kunishambulia bila kisa. Ingawa niliwapenda, walinishtaki, hata hivyo niliwaombea dua. Wananilipa uovu kwa wema wangu, na chuki kwa mapendo yangu. Umweke hakimu mbaya dhidi ya adui yangu; na mshtaki wake ampeleke mahakamani. Anapohukumiwa apatikane na hatia; lalamiko lake lihesabiwe kuwa kosa jingine. Siku za maisha yake ziwe chache, mtu mwingine na achukue kazi yake! Watoto wake wawe yatima, na mke wake awe mjane! Watoto wake watangetange na kuombaomba; wafukuzwe katika magofu ya nyumba zao! Anayemdai kitu amnyanganye mali yake yote; na wageni wanyakue mapato ya jasho lake! Pasiwe na mtu wa kumwonea huruma, au Kuwatunza watoto wake yatima! Wazawa wake wote wafe; jina lake lisahauliwe katika kizazi kijacho! Mwenyezi-Mungu aukumbuke uovu wa wazee wake, dhambi za mama yake zisifutwe kamwe! Mwenyezi-Mungu azikumbuke dhambi zao daima; lakini wao wenyewe wasahauliwe duniani. Mwovu huyo hakujali kabisa kuwa na huruma, ila aliwadhulumu maskini na fukara, kadhalika na watu wanyonge mpaka kifo. Yeye alipenda kulaani watu, laana na impate yeye mwenyewe. Hakuwatakia wengine baraka, basi, asipate baraka yeye mwenyewe. Kwake kulaani ni kama kuvaa nguo, basi, laana hizo zimloweshe kama maji, zimwingie mifupani mwake kama mafuta. Laana zimfunike kama nguo, zimzunguke daima kama ukanda. Mwenyezi-Mungu awalipe hayo hao watu wanaonishtaki, naam hao wanaosema mabaya dhidi yangu. Lakini ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wangu, unitendee kadiri ya hisani yako; uniokoe, kwa sababu ya wema wa fadhili zako! Mimi ni maskini na fukara; nimejeruhiwa mpaka moyoni mwangu. Natoweka kama kivuli cha jioni; nimepeperushwa kama nzige. Magoti yangu yamenyongonyea kwa mfungo; nimebaki mifupa na ngozi. Nimekuwa dhihaka tupu kwa watu; wanionapo hutikisa vichwa vyao kwa dharau. Unisaidie, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu; uniokoe kadiri ya fadhili zako. Waoneshe watu kuwa ndiwe uliyetenda hayo, wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe uliyefanya hivyo. Waache walaani, lakini wewe unibariki; wanaonishambulia waaibike, nami mtumishi wako nifurahi. Maadui zangu na wavishwe fedheha; wajifunike aibu yao kama blanketi. Nitamshukuru sana Mwenyezi-Mungu kwa sauti; nitamsifu kati ya kundi kubwa la watu, kwa maana yeye humtetea maskini, humwokoa wakati anapohukumiwa. (Zaburi ya Daudi) Mwenyezi-Mungu amwambia bwana wangu: “Keti upande wangu wa kulia, hata niwaweke maadui zako chini ya miguu yako.” Mwenyezi-Mungu ataeneza enzi yako kutoka Siyoni; utatawala juu ya maadui zako wote. Watu wako watakujia kwa hiari, siku utakapokwenda kuwapiga maadui. Juu ya milima mitakatifu watakujia vijana wako, kama umande unaotokeza alfajiri mapema. Mwenyezi-Mungu amekuapia wala hatabadili nia yake: “Wewe ni kuhani milele kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.” Bwana yuko upande wako wa kulia; atawaponda wafalme atakapokasirika. Atayahukumu mataifa na kuwaua watu wengi; atawaponda viongozi kila mahali duniani. Mfalme atakunywa maji ya kijito njiani; naye atainua kichwa juu kwa ushindi. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Nitamshukuru Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote, nikijumuika na jamii ya watu waadilifu. Matendo ya Mwenyezi-Mungu ni makuu mno! Wote wanaoyafurahia huyatafakari. Kila afanyacho kimejaa utukufu na fahari; uadilifu wake wadumu milele. Amesababisha matendo yake ya ajabu yakumbukwe; Mwenyezi-Mungu ni mwema na mwenye huruma. Huwapa chakula wenye kumcha; hasahau kamwe agano lake. Amewaonesha watu wake nguvu ya matendo yake, amewapa nchi za mataifa mengine ziwe mali yao. Matendo yake ni ya haki na ya kuaminika; kanuni zake zote ni za kutegemewa. Amri zake zadumu daima na milele; zimetolewa kwa haki na uadilifu. Aliwakomboa watu wake na kufanya nao agano la milele. Yeye ni mtakatifu na wa kutisha mno! Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa hekima; wote wanaozitii amri zake hujaliwa busara. Sifa zake zadumu milele. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Heri mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu, anayefurahia sana kutii amri zake. Wazawa wake watakuwa wenye nguvu nchini; watoto wa wanyofu watapata baraka. Nyumbani kwake kutakuwa na mali nyingi; uadilifu wake wadumu milele. Mtu mwema huangaziwa mwanga gizani; mtu mwenye huruma, mpole na mwadilifu. Mtu mkarimu akopeshaye bila faida, hufanikiwa; mtu afanyaye shughuli zake kwa kutumia haki. Mwadilifu hatashindwa kamwe, huyo atakumbukwa milele. Hana haja ya kuogopa akipata habari mbaya; ana moyo thabiti na humtegemea Mwenyezi-Mungu. Yuko imara moyoni, wala hataogopa; naye atawaona maadui zake wanashindwa. Hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini; uadilifu wake wadumu milele. Nguvu yake inatukuzwa kwa heshima. Watu waovu huona hayo na kuudhika; husaga meno kwa chuki na kutoweka, matazamio ya mtu mbaya huishia patupu. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Enyi watumishi wa Mwenyezi-Mungu, lisifuni jina lake! Jina lake litukuzwe, sasa na hata milele. Kutoka mashariki na hata magharibi, litukuzwe jina la Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu atawala juu ya mataifa yote, utukufu wake wafika juu ya mbingu. Nani aliye kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu? Yeye ameketi juu kabisa; lakini anatazama chini, azione mbingu na dunia. Humwinua fukara kutoka mavumbini; humnyanyua maskini kutoka unyonge wake, na kumweka pamoja na wakuu; pamoja na wakuu wa watu wake. Humjalia mwanamke tasa furaha nyumbani kwake; humfurahisha kwa kumjalia watoto. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Watu wa Israeli walipotoka Misri, wazawa wa Yakobo walipotoka ugenini, Yuda ikawa maskani ya Mungu, Israeli ikawa milki yake. Bahari iliona hayo ikakimbia; mto Yordani ukaacha kutiririka! Milima ilirukaruka kama kondoo dume; vilima vikaruka kama wanakondoo! Ee bahari, imekuwaje hata ukakimbia? Nawe Yordani, kwa nini ukaacha kutiririka? Enyi milima, mbona mliruka kama kondoo dume? Nanyi vilima, mmerukaje kama wanakondoo? Tetemeka, ee dunia mbele yake Mwenyezi-Mungu; tetemeka mbele ya Mungu wa Yakobo, anayeugusa mwamba ukawa bwawa la maji, nayo majabali yakawa chemchemi za maji! Sio sisi, ee Mwenyezi-Mungu, sio sisi; bali wewe peke yako utukuzwe, kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako. Kwa nini mataifa yaseme: “Mungu wenu yuko wapi?” Mungu wetu yuko mbinguni; yeye hufanya yote anayotaka. Miungu yao ni ya fedha na dhahabu; imetengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Ina vinywa, lakini haisemi. Ina macho, lakini haioni. Ina masikio, lakini haisikii. Ina pua, lakini hainusi. Ina mikono, lakini haipapasi. Ina miguu, lakini haitembei. Haiwezi kamwe kutoa sauti. Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo, kadhalika na wote wanaoitumainia. Enyi Waisraeli, mtumainieni Mwenyezi-Mungu; yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu. Enyi wazawa wa Aroni, mtumainieni Mwenyezi-Mungu; yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu. Enyi mnaomcha Mwenyezi-Mungu, mtumainini, yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu. Mwenyezi-Mungu atukumbuka na atatubariki; atawabariki watu wa Israeli, atawabariki wazawa wa Aroni. Atawabariki wote wamchao, atawabariki wakubwa na wadogo. Mwenyezi-Mungu awajalieni muongezeke; awajalieni muongezeke nyinyi na wazawa wenu! Mbarikiwe na Mwenyezi-Mungu, aliyeziumba mbingu na dunia. Mbingu ni mali yake Mwenyezi-Mungu, bali dunia amewapa binadamu. Wafu hawamsifu Mwenyezi-Mungu, wala wale wanaoshuka katika nchi ya kimya. Lakini sisi tulio hai twamsifu Mwenyezi-Mungu; tutamsifu sasa na hata milele. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Nampenda Mwenyezi-Mungu, kwa maana anisikia, maana amesikia kilio cha ombi langu. Yeye amenitegea sikio, hivyo nitamwomba muda wote niishio. Hatari ya kifo ilinizunguka, vitisho vya kaburi vilinivamia; nilijawa na mahangaiko na majonzi. Kisha nikamlilia Mwenyezi-Mungu: “Ee Mwenyezi-Mungu, tafadhali unisalimishe!” Mwenyezi-Mungu amejaa wema na uaminifu; Mungu wetu ni mwenye huruma. Mwenyezi-Mungu huwalinda wanyofu; nilipokuwa nimekandamizwa aliniokoa. Uwe na utulivu mkuu, ee nafsi yangu, maana Mwenyezi-Mungu amenitendea mema. Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu; akanilinda nisije nikaanguka. Nitatembea mbele yake Mwenyezi-Mungu, katika nchi ya watu walio hai. Nilikuwa na imani hata niliposema: “Mimi nimetaabika mno.” Hata nilisema kwa hofu yangu: “Binadamu wote hawaaminiki!” Nimrudishie nini Mwenyezi-Mungu, kwa ukarimu wote alionitendea? Nitamtolea tambiko ya divai kwa kunikomboa, nitaomba kwa jina lake Mwenyezi-Mungu. Nitamtimizia Mwenyezi-Mungu nadhiri zangu, mbele ya watu wake wote. Kifo cha waaminifu wake Mwenyezi-Mungu si jambo dogo mbele yake. Ee Mwenyezi-Mungu, mimi ni mtumishi wako; ni mtumishi wako, mtoto wa mjakazi wako; umenifungulia vifungo vyangu. Nitakutolea tambiko za shukrani, na kukupa heshima zangu. Nitakutimizia ahadi zangu, ee Mwenyezi-Mungu mbele ya watu wako wote, waliokusanyika hekaluni mwako, katikati ya Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Enyi mataifa yote, msifuni Mwenyezi-Mungu! Enyi watu wote mhimidini! Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu; uaminifu wake Mwenyezi-Mungu wadumu milele! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele. Watu wa Israeli na waseme: “Fadhili zake zadumu milele.” Wazawa wa Aroni na waseme: “Fadhili zake zadumu milele.” Wote wamchao Mwenyezi-Mungu na waseme: “Fadhili zake zadumu milele.” Katika taabu yangu nilimwomba Mwenyezi-Mungu, naye akanisikia na kuniweka huru. Mwenyezi-Mungu yuko nami, siogopi kitu; binadamu ataweza kunifanya nini? Mwenyezi-Mungu yuko nami, kunisaidia; nami nitawaona maadui zangu wameshindwa. Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu, kuliko kumtumainia mwanadamu. Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu, kuliko kuwatumainia viongozi wa dunia. Mataifa yote yalinizingira, lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu nikayaangamiza! Yalinizunguka kila upande, lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu, nikayaangamiza! Yalinizunguka, mengi kama nyuki, lakini yakateketea kama kichaka motoni; kwa jina la Mwenyezi-Mungu niliyaangamiza! Nilishambuliwa mno karibu nishindwe, lakini Mwenyezi-Mungu alinisaidia. Mwenyezi-Mungu ni nguvu yangu kuu; yeye mwenyewe ndiye wokovu wangu. Sauti za furaha ya ushindi zasikika hemani mwao waadilifu: “Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu! Mkono wa nguvu wa Mwenyezi-Mungu umeleta ushindi! Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!” Sitakufa, bali nitaishi, na kusimulia matendo ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu ameniadhibu sana, lakini hakuniacha nife. Nifungulie milango ya watu waadilifu, niingie na kumshukuru Mwenyezi-Mungu! Huu ndio mlango wa Mwenyezi-Mungu, watu waadilifu watapitia humo. Nakushukuru, ee Mungu kwa kunijibu; kwa sababu wewe ni wokovu wangu. Jiwe walilokataa waashi, limekuwa jiwe kuu la msingi. Hiyo ni kazi yake Mwenyezi-Mungu nayo ni ya ajabu sana kwetu. Hii ndiyo siku aliyoifanya Mwenyezi-Mungu; tushangilie na kufurahi. Tafadhali utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu! Tafadhali utufanikishe, ee Mwenyezi-Mungu! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mwenyezi-Mungu! Twawabariki kutoka nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu Mwenyezi-Mungu ni Mungu; yeye ametujalia mwanga wake Shikeni matawi ya sherehe, mkiandamana mpaka madhabahuni. Wewe ni Mungu wangu, nami ninakushukuru; ninakutukuza, ee Mungu wangu. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele. Heri watu wanaoishi bila kosa, wanaozingatia sheria ya Mwenyezi-Mungu. Heri wanaozingatia matakwa yake, wanaomtafuta kwa moyo wao wote, watu wasiotenda uovu kamwe, bali daima hufuata njia zake. Ee Mungu, umetupatia kanuni zako ili tuzishike kwa uaminifu. Laiti mwenendo wangu ungeimarika, kwa kuyafuata masharti yako! Nikizingatia amri zako zote, hapo kweli sitaaibishwa. Nitakusifu kwa moyo mnyofu, nikijifunza maagizo yako maadilifu. Nitayafuata masharti yako; usiniache hata kidogo. Kijana atatunzaje maisha yake kuwa safi? Kwa kuyaongoza kadiri ya neno lako. Najitahidi kukutii kwa moyo wote; usiniache nikiuke amri zako. Nimeshika neno lako moyoni mwangu, nisije nikakukosea. Utukuzwe, ee Mwenyezi-Mungu! Unifundishe masharti yako. Nitayarudia kwa sauti maagizo yako yote uliyotoa. Nafurahi kufuata maamuzi yako, kuliko kuwa na utajiri mwingi. Nazitafakari kanuni zako, na kuzizingatia njia zako. Nayafurahia masharti yako; sitalisahau neno lako. Unitendee mimi mtumishi wako kwa ukarimu, nipate kuishi na kushika neno lako. Uyafumbue macho yangu, niyaone maajabu ya sheria yako. Mimi ni mkimbizi tu hapa duniani; usinifiche amri zako. Roho yangu yaugua kwa hamu kubwa ya kutaka kujua daima maagizo yako. Wewe wawakemea wenye kiburi, walaanifu, ambao wanakiuka amri zako. Uniepushe na matusi na madharau yao, maana nimeyazingatia maamuzi yako. Hata kama wakuu wanakula njama dhidi yangu; mimi mtumishi wako nitayatafakari maamuzi yako. Masharti yako ni furaha yangu; hayo ni washauri wangu. Nagaagaa chini mavumbini; unipe tena uhai kama ulivyoahidi. Nimeungama niliyotenda, nawe ukanijibu; unifundishe masharti yako. Unifundishe namna ya kushika kanuni zako, nami nitayatafakari matendo yako ya ajabu. Niko hoi kwa uchungu; unirudishie nguvu kama ulivyoahidi. Uniepushe na njia za upotovu; unifundishe kwa wema sheria yako. Nimechagua njia ya uaminifu; nimezingatia maagizo yako. Nazingatia maamuzi yako, ee Mwenyezi-Mungu; usikubali niaibishwe! Nitafuata maelekezo ya amri zako, maana unanipa maarifa zaidi. Ee Mwenyezi-Mungu, unifundishe kutii masharti yako; nami nitayashika mpaka mwisho. Unieleweshe nipate kuishika sheria yako, niifuate kwa moyo wangu wote. Uniongoze katika njia ya amri zako, maana humo napata furaha yangu. Unipe ari ya kuzingatia maamuzi yako, na si kwa ajili ya kupata faida isiyofaa. Uniepushe, nisifuate mambo ya upuuzi; unioneshe njia yako, unipe uhai. Unitimizie mimi mtumishi wako ahadi yako; ahadi unayowapa wale wanaokuheshimu. Uniokoe na lawama ninazoogopa; maana maagizo yako ni mema. Natamani sana kuzitii kanuni zako; unijalie uhai maana wewe ni mwadilifu. Fadhili zako zinijie, ee Mwenyezi-Mungu; uniokoe kama ulivyoahidi. Hapo nitaweza kuwajibu hao wanaonitukana, maana mimi nina imani sana na neno lako. Unijalie kusema ukweli wako daima, maana tumaini langu liko katika maagizo yako. Nitatii sheria yako daima, nitaishika milele na milele. Nitaishi katika uhuru kamili, maana nazitilia maanani kanuni zako. Nitawatangazia wafalme maamuzi yako, wala sitaona aibu. Furaha yangu ni kuzitii amri zako, ambazo mimi nazipenda. Naziheshimu na kuzipenda amri zako; nitayatafakari masharti yako. Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mtumishi wako, ahadi ambayo imenipa matumaini. Hata niwapo taabuni napata kitulizo, maana ahadi yako yanipa uhai. Wasiomjali Mungu hunidharau daima, lakini mimi sikiuki sheria yako. Ninapoyakumbuka maagizo yako ya tangu kale, nafarijika, ee Mwenyezi-Mungu. Nashikwa na hasira kali, nionapo waovu wakivunja sheria yako. Masharti yako yamekuwa wimbo wangu, nikiwa huku ugenini. Usiku ninakukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu, na kushika sheria yako. Hii ni baraka kubwa kwangu, kwamba nazishika kanuni zako. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe riziki yangu kuu; naahidi kushika maneno yako. Naomba radhi yako kwa moyo wangu wote; unionee huruma kama ulivyoahidi! Nimeufikiria mwenendo wangu, na nimerudi nifuate maamuzi yako. Bila kukawia nafanya haraka kuzishika amri zako. Waovu wametega mitego waninase, lakini mimi sisahau sheria yako. Usiku wa manane naamka kukusifu, kwa sababu ya maagizo yako maadilifu. Mimi ni rafiki ya wote wakuchao, rafiki yao wanaozitii kanuni zako. Dunia imejaa fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, unifundishe masharti yako. Umenitendea vema mimi mtumishi wako, kama ulivyoahidi, ee Mwenyezi-Mungu. Unifundishe akili na maarifa, maana nina imani sana na amri zako. Kabla ya kuniadhibu nilikuwa nikikosea, lakini sasa nashika neno lako. Wewe ni mwema na mfadhili; unifundishe masharti yako. Wenye kiburi wanasema uongo juu yangu, lakini mimi nashika kanuni zako kwa moyo wote. Mioyo yao imejaa upumbavu, lakini mimi nafurahia sheria yako. Nimefaidika kutokana na taabu yangu, maana imenifanya nijifunze masharti yako. Sheria uliyoweka ni bora kwangu, kuliko mali zote za dunia. Mikono yako iliniumba na kuniunda; unijalie akili nijifunze amri zako. Wakuchao wataniona na kufurahi, maana tumaini langu liko katika neno lako. Najua hukumu zako ni adili, ee Mwenyezi-Mungu, na kwamba umeniadhibu kwani wewe ni mwaminifu. Fadhili zako na zinipe faraja, kama ulivyoniahidi mimi mtumishi wako. Unionee huruma nipate kuishi, maana sheria yako ni furaha yangu. Wenye kiburi waaibike kwa maana wamenifanyia hila, lakini mimi nitazitafakari kanuni zako. Wote wakuchao na waje kwangu, wapate kuyajua maamuzi yako. Moyo wangu na uzingatie masharti yako, nisije nikaaibishwa. Niko hoi kwa kukungojea uniokoe; naweka tumaini langu katika neno lako. Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi. Nauliza: “Utakuja lini kunifariji?” Nimekunjamana kama kiriba katika moshi, hata hivyo sijasahau masharti yako. Mimi mtumishi wako nitasubiri mpaka lini? Utawaadhibu lini wale wanaonidhulumu? Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, watu ambao hawafuati sheria yako. Amri zako zote ni za kuaminika; watu wananitesa bila haki; unisaidie! Karibu wangefaulu kuniangamiza, lakini mimi sijavunja kanuni zako. Unisalimishe kadiri ya fadhili zako, nipate kuzingatia maamuzi uliyotamka. Neno lako, ee Mwenyezi-Mungu, ladumu milele; limethibitika juu mbinguni. Uaminifu wako wadumu vizazi vyote, umeiweka dunia mahali pake nayo yadumu. Kwa amri yako viumbe vyote vipo leo, maana vitu vyote ni watumishi wako. Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu, ningalikwisha angamia kwa taabu zangu. Sitasahau kamwe kanuni zako, maana kwa hizo umenipa uhai. Mimi ni wako, uniokoe, maana nimejitahidi kuzishika kanuni zako. Waovu wanivizia wapate kuniua; lakini mimi natafakari masharti yako. Nimetambua kila kitu hufikia kikomo, lakini amri yako ni kamilifu. Naipenda sana sheria yako! Naitafakari mchana kutwa! Amri yako iko nami daima, yanipa hekima kuliko maadui zangu. Ninaelewa kuliko waalimu wangu wote, kwa kuwa nayatafakari maamuzi yako. Nawapita wazee kwa busara yangu, kwa sababu nazishika kanuni zako. Najizuia nisifuate njia mbaya, nipate kulizingatia neno lako. Sikukiuka maagizo yako, maana wewe mwenyewe ulinifundisha. Maneno yako ni matamu sana kwangu; naam, ni matamu kuliko asali! Kwa kanuni zako napata hekima, kwa hiyo nachukia kila mwenendo mbaya. Neno lako ni taa ya kuniongoza, na mwanga katika njia yangu. Nimeapa na kuthibitisha kiapo changu, kwamba nitashika maagizo yako adili. Ee Mwenyezi-Mungu, ninateseka mno; unijalie uhai kama ulivyoahidi. Ee Mwenyezi-Mungu, upokee sala yangu ya shukrani; na kunifundisha maagizo yako. Maisha yangu yamo hatarini daima, lakini siisahau sheria yako. Waovu wamenitegea mitego, lakini sikiuki kanuni zako. Maamuzi yako ni riziki kubwa kwangu milele; hayo ni furaha ya moyo wangu. Nimekusudia kwa moyo wote kufuata masharti yako milele. Nawachukia watu wanafiki, lakini naipenda sheria yako. Wewe ni ngao yangu, kwako napata usalama; naweka tumaini langu katika neno lako. Ondokeni kwangu, enyi waovu, ili nipate kushika amri za Mungu wangu. Uniimarishe ulivyoahidi, nami nitaishi; usikubali niaibike katika tumaini langu. Unitegemeze, niwe salama; niwe daima msikivu kwa masharti yako. Unawakataa wote wanaokiuka masharti yako; mawazo yao maovu ni ya bure. Waovu wote wawaona kuwa takataka, kwa hiyo mimi napenda maamuzi yako. Natetemeka kwa kukuogopa wewe; nimejaa hofu kwa sababu ya hukumu zako. Nimefanya mambo mema na adili; usiniache makuchani mwa maadui zangu. Uahidi kunisaidia mimi mtumishi wako; usikubali wenye kiburi wanidhulumu. Macho yangu yanafifia nikingojea uniokoe, nikingojea utimize uliyoahidi. Unitendee mimi mtumishi wako kadiri ya wema wako, unifundishe masharti yako. Mimi ni mtumishi wako, unipe maarifa, nipate kujua maamuzi yako. Ee Mwenyezi-Mungu, sasa ni wakati wa kufanya kitu, kwa maana watu wanavunja sheria yako. Mimi, nazipenda amri zako, kuliko hata dhahabu safi kabisa. Kwa hiyo, nafuata kanuni zako zote; kila njia potovu naichukia. Maamuzi yako ni ya ajabu; kwa hiyo nayashika kwa moyo wote. Maelezo ya mafundisho yako huleta mwanga; huwapa akili watu wasiojua kitu. Nafungua kinywa kwa hamu kubwa, maana ninatamani sana amri zako. Unigeukie na kunionea huruma, kama uwatendeavyo wanaokupenda. Uniimarishie hatua zangu kama ulivyoahidi; usikubali mimi nitawaliwe na uovu. Unikomboe kutoka udhalimu wa binadamu, ili nipate kuzishika kanuni zako. Uniangazie uso wako kwa wema, unifundishe masharti yako. Macho yangu yabubujika machozi kama mto, kwa sababu watu hawaishiki sheria yako. Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ni mwadilifu; na hukumu zako ni za haki. Umetoa maamuzi yako, kwa haki na uthabiti. Upendo wangu kwako wanifanya niwake hasira, maana maadui zangu hawajali maneno yako. Ahadi yako ni hakika kabisa, nami mtumishi wako naipenda. Mimi ni mdogo na ninadharauliwa; hata hivyo sisahau kanuni zako. Uadilifu wako ni wa haki milele; sheria yako ni ya kweli. Taabu na huzuni vimenipata, lakini amri zako ndizo furaha yangu. Maamuzi yako ni ya haki daima; unijalie maarifa nipate kuishi. Nakulilia kwa moyo wangu wote; unijibu, ee Mwenyezi-Mungu, nifuate kanuni zako. Nakulilia, unisalimishe; nipate kuyazingatia maamuzi yako. Naamka kabla ya pambazuko na kukuomba msaada; naweka tumaini langu katika maneno yako. Nakaa macho usiku kucha, ili nitafakari juu ya maagizo yako. Kwa fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, unisikie; unisalimishe kwa uadilifu wako. Wale wanaonidhulumu vibaya wanakaribia, hao wako mbali kabisa na sheria yako. Lakini wewe u karibu nami, ee Mwenyezi-Mungu, na amri zako zote ni za kuaminika. Tangu zamani, nimejifunza maamuzi yako; ambayo umeyaweka hata yadumu milele. Uangalie mateso yangu, uniokoe, kwa maana sikuisahau sheria yako. Unitetee na kunikomboa; unijalie uhai kama ulivyoahidi. Waovu hawataokolewa kamwe, maana hawajali juu ya masharti yako. Huruma yako ni kubwa, ee Mwenyezi-Mungu, unijalie uhai kama ulivyoahidi. Maadui na wadhalimu wangu ni wengi, lakini mimi sikiuki maamuzi yako. Niwaonapo wahaini hao nachukizwa mno, kwa sababu hawazishiki amri zako. Tazama, ee Mungu, ninavyozipenda kanuni zako! Unijalie uhai kadiri ya fadhili zako. Kitovu cha neno lako ni ukweli, maagizo yako yote adili, yadumu milele. Wakuu wanidhulumu bila kisa, lakini mimi naheshimu maneno yako kwa moyo wote. Nafurahi kwa sababu ya neno lako, kama mtu aliyekuta kitu cha thamani kuu. Nachukia kabisa uongo, lakini naipenda sheria yako. Nakusifu mara saba kila siku, kwa sababu ya maagizo yako adili. Wapendao sheria yako wana amani kuu; hakuna kinachoweza kuwaangusha. Ee Mwenyezi-Mungu, nakungojea uniokoe; mimi natimiza amri zako. Nazingatia maamuzi yako; nayapenda kwa moyo wote. Nazingatia kanuni na maamuzi yako; wewe wauona mwenendo wangu wote. Kilio changu kikufikie, ee Mwenyezi-Mungu! Unijalie akili kama ulivyoahidi. Ombi langu likufikie; uniokoe kama ulivyoahidi. Nitasema sifa zako mfululizo, maana wanifundisha masharti yako. Nitaimba juu ya neno lako, maana amri zako zote ni za haki. Uwe daima tayari kunisaidia, maana nimeamua kufuata kanuni zako. Natazamia sana uniokoe, ee Mwenyezi-Mungu; sheria yako ndiyo furaha yangu. Unijalie kuishi nipate kukusifu; na maagizo yako yanisaidie. Natangatanga kama kondoo aliyepotea; uje kunitafuta mimi mtumishi wako, maana sikusahau amri zako. (Wimbo wa Kwenda Juu ) Katika taabu yangu nilimwita Mwenyezi-Mungu, naye akanijibu. Uniokoe ee Mwenyezi-Mungu, na watu wadanganyifu na waongo. Enyi watu wadanganyifu, mtapewa kitu gani? Mtaadhibiwa namna gani? Kwa mishale mikali ya askari, kwa makaa ya moto mkali! Ole wangu kwamba naishi kama mgeni huko Mesheki; naishi kama mgeni katika mahema ya Kedari. Nimeishi muda mrefu mno kati ya watu wanaochukia amani! Wakati ninaposema nataka amani, wao wanataka tu vita. (Wimbo wa Kwenda Juu, wa Daudi) Natazama juu milimani; msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia. Hatakuacha uanguke; mlinzi wako hasinzii. Kweli mlinzi wa Israeli hasinzii wala halali. Mwenyezi-Mungu ni mlinzi wako; yuko upande wako wa kulia kukukinga. Mchana jua halitakuumiza, wala mwezi wakati wa usiku. Mwenyezi-Mungu atakukinga na baya lolote; atayalinda salama maisha yako. Mwenyezi-Mungu atakulinda katika shughuli zako zote tangu sasa na hata milele. (Wimbo wa Kwenda Juu, wa Daudi) Nilifurahi waliponiambia: “Twende nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu.” Sasa tuko tumesimama, kwenye malango yako, ee Yerusalemu! Yerusalemu, mji uliojengwa, ili jumuiya ikutane humo. Humo ndimo makabila yanamofika, naam, makabila ya Israeli, kumshukuru Mwenyezi-Mungu kama alivyoagiza. Humo mmewekwa mahakama ya hukumu ya haki, mahakama ya ukoo wa kifalme wa Daudi. Uombeeni Yerusalemu amani: “Wote wakupendao na wafanikiwe! Ndani ya kuta zako kuwe na amani, majumbani mwako kuweko usalama!” Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu, ee Yerusalemu, nakutakia amani! Kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ninakuombea upate fanaka! (Wimbo wa Kwenda Juu) Nakutazamia kwa hamu, ee Mwenyezi-Mungu, nakuangalia wewe utawalaye huko juu mbinguni! Kama watumishi wamtegemeavyo bwana wao, kama mjakazi amtegemeavyo bibi yake, ndivyo nasi tunavyokutegemea wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mpaka hapo utakapotuonea huruma. Utuhurumie, ee Mwenyezi-Mungu, utuhurumie, maana tumedharauliwa kupita kiasi. Tumeshiba muda mrefu dharau za matajiri, tumepuuzwa mno na wenye kiburi. (Wimbo wa Kwenda Juu, wa Daudi) “Kama Mwenyezi-Mungu asingalikuwa upande wetu Semeni nyote mlio katika Israeli: “Kama Mwenyezi-Mungu asingalikuwa upande wetu, wakati ule tuliposhambuliwa na maadui, hakika tungalimezwa tukiwa hai, wakati hasira zao zilipotuwakia. Tungalikumbwa na gharika, tungalifunikwa na mto wa maji, mkondo wa maji ungalituchukua!” Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, ambaye hakutuacha makuchani mwao. Tumeponyoka kama ndege mtegoni; mtego umeteguliwa, nasi tukaokoka. Msaada wetu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia. (Wimbo wa Kwenda Juu) Wanaomtegemea Mwenyezi-Mungu, wako kama mlima Siyoni, ambao hautikisiki bali wabaki imara daima. Kama Yerusalemu inavyozungukwa na milima, ndivyo Mwenyezi-Mungu awazungukavyo watu wake, tangu sasa na hata milele. Waovu hawataendelea kutawala nchi ya waadilifu; wasije waadilifu nao wakafanya maovu. Ee Mwenyezi-Mungu, uwe mwema kwa watu wema, kwa wale wanaozitii amri zako. Lakini wanaogeuka na kufuata njia zao mbaya uwakumbe pamoja na watenda maovu. Amani iwe na Israeli! (Wimbo wa Kwenda Juu) Mwenyezi-Mungu alipoturekebisha na kuturudisha Siyoni, tulikuwa kama watu wanaoota ndoto! Hapo tuliangua kicheko; tulishangilia kwa furaha. Nao watu wa mataifa mengine walisema: “Mwenyezi-Mungu amewatendea mambo makubwa!” Kweli Mwenyezi-Mungu alitutendea mambo makubwa, tulifurahi kwelikweli! Ee Mwenyezi-Mungu, urekebishe tena hali yetu, kama mvua inavyotiririsha maji katika mabonde makavu. Wanaopanda kwa machozi, watavuna kwa shangwe. Wanaokwenda kupanda mbegu wakilia, watarudi kwa furaha wakichukua mavuno. (Wimbo wa Kwenda Juu, wa Solomoni) Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba, waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure. Mnajisumbua bure kuamka mapema asubuhi na kuchelewa kwenda kupumzika jioni, mjipatie chakula kwa jasho lenu. Mungu huwaruzuku walio wake hata walalapo. Watoto ni riziki kutoka kwa Mwenyezi-Mungu; watoto ni tuzo lake kwetu sisi. Watoto waliozaliwa wazazi wakiwa bado vijana, ni kama mishale mikononi mwa askari. Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi. Hatashindwa atakapokabiliana na adui mahakamani. (Wimbo wa Kwenda Juu) Heri wote wamchao Mwenyezi-Mungu, wanaoishi kufuatana na amri zake. Utapata matunda ya jasho lako, utafurahi na kupata fanaka. Mkeo atakuwa kama mzabibu wa matunda mengi nyumbani mwako; watoto wako kama chipukizi za mzeituni kuzunguka meza yako. Naam, ndivyo atakavyobarikiwa mtu amchaye Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akubariki kutoka Siyoni! Uione fanaka ya Yerusalemu, siku zote za maisha yako. Uishi na hata uwaone wajukuu zako! Amani iwe na Israeli! (Wimbo wa Kwenda Juu) “Nimesumbuliwa vibaya tangu ujana wangu Kila mtu katika Israeli na aseme: “Nimesumbuliwa vibaya tangu ujana wangu, lakini hawakufaulu kunishinda. Walinijeruhi vibaya mgongoni mwangu, wakafanya kama mkulima anayelima shamba. Lakini Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu; amezikata kamba za hao watu waovu.” Na waaibishwe na kurudishwa nyuma, wote wale wanaouchukia mji wa Siyoni. Wawe kama nyasi juu ya paa la nyumba, ambazo hunyauka kabla hazijakua, hakuna anayejishughulisha kuzikusanya, wala kuzichukua kama matita. Hakuna apitaye karibu atakayewaambia: “Mwenyezi-Mungu awabariki! Twawabariki kwa jina la Mwenyezi-Mungu!” (Wimbo wa Kwenda Juu) Toka upeo wa unyonge wangu, nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu. Ee Bwana, sikia sauti yangu, uitegee sikio sauti ya ombi langu. Kama, ee Mwenyezi-Mungu ungekumbuka maovu yetu nani, ee Bwana, angeweza kusalimika? Lakini kwako twapata msamaha, ili sisi tukuheshimu. Namtumainia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote; nina imani sana na neno lake. Ninamtumainia Mwenyezi-Mungu kuliko walinzi wanavyongojea pambazuko; kuliko walinzi wanavyongojea kuche asubuhi. Ee Israeli, umtumainie Mwenyezi-Mungu, maana kwake Mwenyezi-Mungu kuna fadhili, kwake kuna nguvu kubwa ya kutukomboa. Yeye atawakomboa watu wa Israeli kutoka katika maovu yao yote. (Wimbo wa Kwenda Juu, wa Daudi) Ee Mwenyezi-Mungu, sina moyo wa kiburi; mimi si mtu wa majivuno. Sijishughulishi na mambo makuu, au yaliyo ya ajabu mno kwangu. Ila nafsi yangu imetulia na kuwa na amani, kama mtoto mchanga alivyotulia na mama yake; ndivyo nafsi yangu ilivyo tulivu. Ee Israeli, umtumainie Mwenyezi-Mungu, tangu sasa na hata milele. (Wimbo wa Kwenda Juu) Ee Mwenyezi-Mungu, mkumbuke Daudi, kumbuka taabu zote alizopata. Ukumbuke ahadi aliyokupa, ee Mwenyezi-Mungu, kiapo alichokuapia, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo: “Sitaingia ndani ya nyumba yangu, wala kulala kitandani mwangu; sitakubali kulala usingizi, wala kusinzia; mpaka nikupatie wewe Mwenyezi-Mungu mahali pa kukaa, makao yako, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo!” Huko Efratha tulisikia habari za sanduku la agano, tukalikuta katika mashamba ya Yearimu. “Haya! Twende nyumbani kwa Mungu, tuabudu mbele ya kiti chake cha enzi!” Inuka ee Mwenyezi-Mungu, nenda kwenye maskani yako; inuka pamoja na sanduku la agano la uwezo wako! Makuhani wako wawe waadilifu daima; na waaminifu wako wapige vigelegele vya furaha! Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako, usimkatae huyo mfalme uliyemweka wakfu. Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi kiapo thabiti, kiapo ambacho hatakibatilisha: “Nitamtawaza mmoja wa wazawa wako mwenyewe, kuwa mfalme baada yako. Watoto wako wakishika agano langu, na kuzingatia mafundisho nitakayowapa, watoto wao pia watakuwa wafalme kama wewe.” Mwenyezi-Mungu ameuchagua mji wa Siyoni, ametaka uwe makao yake: “Hapa ndipo nitakapokaa milele, ndipo maskani yangu maana nimepachagua. Nitaubariki sana mji wa Siyoni kwa mahitaji yake; nitawashibisha chakula maskini wake. Nitawafanikisha makuhani wake kwa wokovu; waaminifu wake watapiga vigelegele vya furaha. Humo nitamchipusha mfalme shujaa wa ukoo wa Daudi: Kama taa iwakayo nitamtegemeza mfalme niliyemteua. Maadui zake nitawavika aibu; lakini yeye nitamvika fahari ya kifalme.” (Wimbo wa Kwenda Juu, wa Daudi) Ni jambo zuri na la kupendeza sana ndugu kuishi pamoja kwa umoja. Ni kama mafuta mazuri yatiririkayo kichwani, mpaka kwenye ndevu zake Aroni, mpaka upindoni mwa vazi lake shingoni. Ni kama umande wa mlima Hermoni, uangukao juu ya vilima vya Siyoni! Huko Mwenyezi-Mungu ameahidi kuwabariki watu wake, kuwapa uhai usio na mwisho. (Wimbo wa Kwenda Juu) Njoni kumsifu Mwenyezi-Mungu enyi watumishi wake wote, enyi nyote mnaotumikia usiku nyumbani mwake. Inueni mikono kuelekea mahali patakatifu, na kumtukuza Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu awabariki kutoka Siyoni; yeye aliyeumba mbingu na dunia. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu, msifuni enyi watumishi wake. Msifuni enyi mkaao katika nyumba yake, ukumbini mwa nyumba ya Mungu wetu! Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; mtukuzeni kwa nyimbo maana inafaa. Mwenyezi-Mungu amemchagua Yakobo kuwa wake, nyinyi watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe. Najua hakika kuwa Mwenyezi-Mungu ni mkuu; Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote. Mwenyezi-Mungu hufanya chochote anachotaka, mbinguni, duniani, baharini na vilindini. Ndiye aletaye mawingu kutoka mipaka ya dunia; afanyaye gharika kuu kwa umeme, na kuvumisha upepo kutoka ghala zake. Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza huko Misri, wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika. Ndiye aliyefanya ishara na maajabu kwako, ee Misri, dhidi ya Farao na maofisa wake wote. Ndiye aliyeyaangamiza mataifa mengi, akawaua wafalme wenye nguvu: Kina Sihoni mfalme wa Waamori, Ogu mfalme wa Bashani, na wafalme wote wa Kanaani. Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake; naam, ziwe riziki ya watu wake Israeli. Jina lako, ee Mwenyezi-Mungu, ladumu milele, utakumbukwa kwa fahari nyakati zote. Mwenyezi-Mungu atawatetea watu wake; na kuwaonea huruma watumishi wake. Miungu ya uongo ya mataifa ni fedha na dhahabu, imetengenezwa kwa mikono ya binadamu. Ina vinywa, lakini haisemi; ina macho, lakini haioni. Ina masikio, lakini haisikii; wala haiwezi hata kuvuta pumzi. Wote walioifanya wafanane nayo, naam, kila mmoja anayeitegemea! Enyi watu wa Israeli, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu! Enyi makuhani, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu! Enyi Walawi, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu! Enyi wachaji wa Mwenyezi-Mungu, mtukuzeni! Atukuzwe Mwenyezi-Mungu katika Siyoni, atukuzwe katika makao yake Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Mshukuruni Mungu wa miungu; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Mshukuruni Bwana wa mabwana; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ndiye peke yake atendaye makuu ya ajabu; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ndiye aliyeziumba mbingu kwa hekima; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ndiye aliyeitengeneza nchi juu ya vilindi vya maji; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ndiye aliyeumba jua, mwezi na nyota; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Jua liutawale mchana; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Mwezi na nyota vitawale usiku; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza wa Misri; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Akawaondoa watu wa Israeli kutoka huko; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Kwa mkono wake wenye nguvu na enzi; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ndiye aliyeigawa Bahari ya Shamu sehemu mbili; kwa maana fadhili zake zadumu milele, akawapitisha watu wa Israeli humo; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Lakini akawazamisha humo Farao na jeshi lake; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ndiye aliyewaongoza watu wake jangwani; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ndiye aliyewapiga wafalme wenye nguvu; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Akawaua wafalme maarufu; kwa maana fadhili zake zadumu milele; akamuua Sihoni, mfalme wa Waamori, kwa maana fadhili zake zadumu milele; na Ogu, mfalme wa Bashani; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Akachukua nchi zao akawapa watu wake; kwa maana fadhili zake zadumu milele; ziwe riziki ya Israeli, mtumishi wake; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ndiye aliyetukumbuka wakati wa unyonge wetu; kwa maana fadhili zake zadumu milele; akatuokoa kutoka maadui zetu; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ndiye akipaye kila kiumbe chenye uhai chakula; kwa maana fadhili zake zadumu milele. Mshukuruni Mungu wa mbinguni; kwa maana fadhili zake zadumu milele! Kando ya mito ya Babuloni, tulikaa, tukawa tunalia tulipokumbuka Siyoni. Katika miti ya nchi ile, tulitundika zeze zetu. Waliotuteka walitutaka tuwaimbie; watesi wetu walitutaka tuwafurahishe: “Tuimbieni mojawapo ya nyimbo za Siyoni!” Twawezaje kuimba wimbo wa Mwenyezi-Mungu katika nchi ya kigeni? Ee Yerusalemu, kama nikikusahau, mkono wangu wa kulia na ukauke! Ulimi wangu na uwe mzito, kama nisipokukumbuka wewe, ee Yerusalemu; naam, nisipokuthamini kuliko furaha yangu kubwa! Ee Mwenyezi-Mungu, usisahau waliyotenda Waedomu, siku ile Yerusalemu ilipotekwa; kumbuka waliyosema: “Bomoeni mji wa Yerusalemu! Ngoeni hata na misingi yake!” Ee Babuloni, utaangamizwa! Heri yule atakayekulipiza mabaya uliyotutenda! Heri yule atakayewatwaa watoto wako na kuwapondaponda mwambani! Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kwa moyo wangu wote, naimba sifa zako mbele ya miungu. Ninasujudu kuelekea hekalu lako takatifu; nalisifu jina lako, kwa sababu ya fadhili zako na uaminifu wako; kwa sababu umeweka jina lako na neno lako juu ya kila kitu. Nilipokulilia, wewe ulinijibu; umeniongezea nguvu zangu. Wafalme wote duniani watakusifu, ee Mwenyezi-Mungu, kwa sababu wameyasikia maneno yako. Wataimba sifa za matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, kwa maana utukufu wako ni mkuu. Ingawa wewe ee Mwenyezi-Mungu, uko juu ya wote, unawaangalia kwa wema walio wanyonge; nao wenye kiburi huwaona kutoka mbali. Hata nikikumbana na taabu, wewe wanilinda; waunyosha mkono wako dhidi ya hasira ya maadui zangu wakali; kwa nguvu yako kuu wanisalimisha. Ee Mwenyezi-Mungu, utatimiza yote uliyoniahidi. Fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, zadumu milele. Usisahau kazi ya mkono wako mwenyewe. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenichunguza; wewe wanijua mpaka ndani. Nikiketi au nikisimama, wewe wajua; wajua kutoka mbali kila kitu ninachofikiria. Watambua nikienda au nikipumzika; wewe wazijua shughuli zangu zote. Kabla sijasema neno lolote, wewe, ee Mwenyezi-Mungu, walijua kabisa. Uko kila upande wangu, mbele na nyuma; waniwekea mkono wako kunilinda. Maarifa yako yapita akili yangu; ni makuu mno, siwezi kuyaelewa. Nikimbilie wapi ambako roho yako haiko? Niende wapi ambako wewe huko? Nikipanda juu mbinguni, wewe upo; nikijilaza chini kuzimu, wewe upo. Nikiruka hadi mawio ya jua, au hata mipakani mwa bahari, hata huko upo kuniongoza; mkono wako wa kulia utanitegemeza. Kama ningeliomba giza linifunike, giza linizunguke badala ya mwanga, kwako giza si giza hata kidogo, na usiku wangaa kama mchana; kwako giza na mwanga ni mamoja. Wewe umeniumba, mwili wangu wote; ulinitengeneza tumboni mwa mama yangu. Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu, matendo yako ni ya ajabu; wewe wanijua kabisakabisa. Umbo langu halikufichika kwako nilipotungwa kwa siri na ustadi ndani ya dunia. Wewe uliniona hata kabla sijazaliwa, uliandika kila kitu kitabuni mwako; siku zangu zote ulizipanga, hata kabla ya kuweko ile ya kwanza. Ee Mungu, mawazo yako ni makuu mno; hayawezi kabisa kuhesabika. Ningeyahesabu yangekuwa mengi kuliko mchanga. Niamkapo, bado nipo pamoja nawe. Laiti, ee Mungu, ungewaua watu waovu! Laiti watu wauaji wangeondoka kwangu! Wanasema vibaya juu yako; wanasema maovu juu ya jina lako! Ee Mwenyezi-Mungu, nawachukia wanaokuchukia; nawadharau sana wale wanaokuasi! Maadui zako ni maadui zangu; ninawachukia kabisakabisa. Unichunguze, ee Mungu, unijue moyo wangu, unipime, uyajue mawazo yangu. Uangalie kama mwenendo wangu ni mbaya, uniongoze katika njia ya milele. (Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) Ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe na watu wabaya, unikinge na watu wakatili. Watu hao huwaza mabaya daima, huzusha magomvi kila mara. Ndimi zao hatari kama za nyoka; midomoni mwao mna maneno ya sumu kama ya joka. Ee Mwenyezi-Mungu, unilinde na makucha ya wabaya; unikinge na watu wakatili ambao wamepanga kuniangusha. Wenye kiburi wamenitegea mitego, wametandaza kamba kama wavu, wameficha mitego njiani wanikamate. Namwambia Mwenyezi-Mungu, “Wewe ndiwe Mungu wangu.” Usikilize, ee Mwenyezi-Mungu, sauti ya ombi langu. Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wangu, mkombozi wangu mkuu, umenikinga salama wakati wa vita. Ee Mwenyezi-Mungu, usiwape waovu wanayotaka; wala mipango yao mibaya usiifanikishe. Hao wanaonizingira wanainua vichwa; uovu wa maneno yao uwapate wao wenyewe! Makaa ya moto yawaangukie; watumbukizwe mashimoni, wasiinuke tena. Wanaowasengenya wengine wasifanikiwe katika nchi; uovu uwapate wakatili na kuwaangamiza mara! Najua Mwenyezi-Mungu hutetea kisa cha wanaoteswa, na kuwapatia haki maskini. Hakika waadilifu watalisifu jina lako; wanyofu watakaa kwako. (Zaburi ya Daudi) Nakuita, ee Mwenyezi-Mungu, uje haraka kunisaidia! Uisikilize sauti yangu wakati ninapokuita! Sala yangu uipokee kama ubani; niinuapo mikono yangu kwako unikubali kama tambiko ya jioni. Ee Mwenyezi-Mungu ukilinde kinywa changu, uweke ulinzi mlangoni mwa mdomo wangu. Unikinge nisielekee kufanya mabaya, nisijishughulishe na matendo maovu; nisijiunge na watu watendao mabaya, wala nisishiriki kamwe karamu zao. Afadhali mtu mwema anipige kunionya; lakini sikubali kamwe kusifiwa na wabaya, maana nasali daima dhidi ya maovu yao. Wakuu wao watakapopondwa miambani, ndipo watatambua maneno yangu yalikuwa sawa. Mifupa yao itatawanywa mdomoni pa Kuzimu kama kuni zilizopasuliwa vipandevipande! Bali mimi nakutegemea, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu; ninakimbilia usalama kwako, usiniache hatarini. Unikinge na mitego waliyonitegea, uniepushe na matanzi ya hao watu waovu. Waovu wanaswe katika mitego yao wenyewe, wakati mimi najiendea zangu salama. (Utenzi wa Daudi alipokuwa pangoni. Sala) Namlilia Mwenyezi-Mungu kwa sauti, namsihi Mwenyezi-Mungu kwa sauti yangu. Namwekea malalamiko yangu, namweleza taabu zangu. Ninapokaribia kukata tamaa kabisa, yeye yupo, anajua mwenendo wangu. Maadui wamenitegea mitego njiani mwangu. Nikiangalia upande wa kulia na kungojea, naona hakuna mtu wa kunisaidia; sina tena mahali pa kukimbilia, hakuna mtu anayenijali. Nakulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu! Wewe ni kimbilio langu la usalama; wewe ni riziki yangu kuu katika nchi ya walio hai. Usikilize kilio changu, maana nimekuwa hoi; uniokoe na watesi wangu, maana wamenizidi nguvu. Unitoe humu kifungoni, ili nipate kukushukuru. Watu waadilifu watajiunga nami kwa sababu umenitendea mema mengi. (Zaburi ya Daudi) Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu! Ulitegee sikio ombi langu maana wewe ni mwaminifu; unijibu kwa sababu ya uadilifu wako. Usinitie hukumuni mimi mtumishi wako, maana hakuna yeyote aliye mwadilifu mbele yako. Maadui zangu wamenifuatia; wameniangusha chini kabisa wameniketisha gizani kama mtu aliyekufa zamani. Nimevunjika moyo kabisa; nimekufa ganzi kwa ajili ya woga. Nakumbuka siku zilizopita; natafakari juu ya yote uliyotenda, nawaza na kuwazua juu ya matendo yako. Nakunyoshea mikono yangu kuomba; nina kiu yako kama nchi kavu isiyo na maji. Ee Mwenyezi-Mungu, unijibu haraka; maana nimekata tamaa kabisa! Usijifiche mbali nami, nisije nikawa kama wale washukao kwa wafu. Asubuhi unioneshe fadhili zako, maana nimekuwekea tumaini langu. Unifundishe mwenendo wa kufuata, maana nakuelekezea ombi la moyo wangu. Uniokoe, ee Mwenyezi-Mungu, kutoka maadui zangu, maana kwako nakimbilia usalama. Unifundishe kutimiza matakwa yako, maana wewe ni Mungu wangu! Roho yako nzuri iniongoze katika njia sawa. Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako, uniondoe katika taabu kwa sababu ya uadilifu wako. Kwa sababu ya fadhili zako uwakomeshe maadui zangu, uwaangamize wote wanaonidhulumu; maana mimi ni mtumishi wako. (Zaburi ya Daudi) Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu, anayeipa mikono yangu mazoezi ya vita, na kuvifunza vidole vyangu kupigana. Yeye ni rafiki yangu amini na ngome yangu, kinga yangu na mkombozi wangu; yeye ni ngao yangu, kwake napata usalama; huyashinda mataifa na kuyaweka chini yangu. Ee Mwenyezi-Mungu, mtu ni nini hata umjali? Mwanadamu ni nini hata umfikirie? Binadamu ni kama pumzi tu; siku zake ni kama kivuli kipitacho. Uinamishe mbingu zako, ee Mwenyezi-Mungu, ushuke chini! Uiguse milima nayo itoe moshi! Lipusha umeme, uwatawanye maadui; upige mishale yako, uwakimbize! Unyoshe mkono wako kutoka juu, uniokoe na kuniondoa katika maji haya mengi; uniondoe makuchani mwa wageni, ambao husema maneno ya uongo, hunyosha mkono kushuhudia uongo. Nitakuimbia wimbo mpya, ee Mungu; nitakupigia kinubi cha nyuzi kumi, wewe uwapaye wafalme ushindi, umwokoaye Daudi mtumishi wako! Uniokoe na upanga wa adui katili, uniondoe makuchani mwa wageni, ambao husema maneno ya uongo, hunyosha mkono kushuhudia uongo. Wavulana wetu wakue kikamilifu kama mimea bustanini; binti zetu wawe kama nguzo zilizochongwa kupambia ikulu. Ghala zetu zijae mazao ya kila aina. Kondoo wetu mashambani wazae maelfu kwa maelfu. Mifugo yetu iwe na afya na nguvu; isitupe mimba wala kuzaa kabla ya wakati. Kusiwepo tena udhalimu mitaani mwetu. Heri taifa ambalo limejaliwa hayo! Heri taifa ambalo Mungu wao ni Mwenyezi-Mungu! (Wimbo wa sifa wa Daudi) Nitakutukuza, ee Mungu wangu na mfalme wangu; nitalitukuza jina lako daima na milele. Nitakutukuza kila siku; nitalisifu jina lako daima na milele. Mwenyezi-Mungu ni mkuu, astahili sifa nyingi; ukuu wake hauwezi kuchunguzika. Kizazi hata kizazi, sifa za matendo yako zitasimuliwa, watu watatangaza matendo yako makuu. Nitanena juu ya utukufu na fahari yako, nitayatafakari matendo yako ya ajabu. Watu watatangaza ukuu wa matendo yako ya ajabu, nami nitatangaza ukuu wako. Watatangaza sifa za wema wako mwingi, na kuimba juu ya uadilifu wako. Mwenyezi-Mungu ni mwenye huruma na rehema; hakasiriki ovyo, amejaa fadhili. Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wote, ni mwenye huruma kwa viumbe vyake vyote. Viumbe vyako vyote vitakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, nao waaminifu wako watakutukuza. Watasema juu ya utukufu wa ufalme wako, na kutangaza juu ya nguvu yako kuu, ili kila mtu ajue matendo yako makuu, na fahari tukufu ya ufalme wako. Ufalme wako ni ufalme wa milele; mamlaka yako yadumu vizazi vyote. Mwenyezi-Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake zote, ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu huwategemeza wote wanaoanguka; huwainua wote waliokandamizwa. Viumbe vyote vinakutazama kwa hamu, nawe wavipa chakula chao kwa wakati wake. Waufumbua mkono wako kwa ukarimu, watosheleza mahitaji ya kila kiumbe hai. Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu katika njia zake zote; ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu yuko karibu na wote wanaomwomba, wote wanaomwomba kwa moyo mnyofu. Huwapatia mahitaji yao wote wanaomcha; husikia kilio chao na kuwaokoa. Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wanaompenda; lakini atawaangamiza waovu wote. Nitatangaza sifa za Mwenyezi-Mungu; viumbe vyote vilisifu jina lake takatifu, milele na milele. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu! Nitamsifu Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote; nitamwimbia Mungu wangu muda wote niishipo. Msiwategemee wakuu wa dunia; hao ni binadamu tu, hawawezi kuokoa. Binadamu akitoa pumzi yake ya mwisho, anarudi mavumbini alimotoka; na hapo mipango yake yote hutoweka. Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo, mtu aliyeweka tumaini lake kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, aliyeumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo. Yeye hushika ahadi yake milele. Yeye huwapatia wanaoonewa haki zao, huwapa wenye njaa chakula. Mwenyezi-Mungu huwapa wafungwa uhuru, huwafungua macho vipofu. Mwenyezi-Mungu huwainua waliokandamizwa; huwapenda watu walio waadilifu. Mwenyezi-Mungu huwalinda wageni, huwategemeza wajane na yatima; lakini huipotosha njia ya waovu. Mwenyezi-Mungu atawala milele, Mungu wako, ee Siyoni, ni mfalme vizazi vyote! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Jinsi gani ilivyo vizuri kumwimbia sifa Mungu wetu! Yeye ni mwema na astahili kuimbiwa sifa. Mwenyezi-Mungu anajenga tena mji wa Yerusalemu; anawarudisha Waisraeli waliokuwa uhamishoni. Anawaponya waliovunjika moyo; na kuwatibu majeraha yao. Anaamua idadi itakayokuwako ya nyota, na kuzipa zote majina yao. Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi; maarifa yake hayana kipimo. Mwenyezi-Mungu huwakweza wanyenyekevu, lakini huwatupa waovu mavumbini. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani, mpigieni kinubi Mungu wetu! Yeye hulifunika anga kwa mawingu, huitengenezea nchi mvua, na kuchipusha nyasi vilimani. Huwapa wanyama chakula chao, na kuwalisha makinda ya kunguru yanapolia. Yeye hataki nguvu za farasi, wala hapendezwi na ushujaa wa askari; lakini hupendezwa na watu wamchao, watu wanaotegemea fadhili zake. Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee Yerusalemu! Umsifu Mungu wako, ee Siyoni! Maana yeye huimarisha milango yako, huwabariki watu waliomo ndani yako. Huweka amani mipakani mwako; hukushibisha kwa ngano safi kabisa. Yeye hupeleka amri yake duniani, na neno lake hufikia lengo lake haraka. Hutandaza theluji kama pamba, hutawanya umande kama majivu. Huleta mvua ya mawe kama kokoto na kwa ubaridi wake maji huganda. Kisha hutoa amri, maji hayo yakayeyuka; huvumisha upepo wake, nayo yakatiririka. Humjulisha Yakobo ujumbe wake, na Israeli masharti na maagizo yake. Lakini hakuyatendea hivyo mataifa mengine; watu wengine hawayajui maagizo yake. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mwenyezi-Mungu kutoka mbinguni, msifuni kutoka huko juu mbinguni. Msifuni, enyi malaika wake wote, msifuni, enyi majeshi yake yote. Msifuni, enyi jua na mwezi, msifuni, enyi nyota zote zingaazo. Msifuni, enyi mbingu za juu, na maji yaliyo juu ya mbingu. Vyote vilisifu jina la Mwenyezi-Mungu, maana yeye aliamuru, na vyote vikawa. Yeye aliviweka mahali pao daima, kwa amri ambayo haiwezi kubatilishwa. Msifuni Mwenyezi-Mungu kutoka duniani; enyi majoka ya baharini na vilindini, msifuni. Msifuni enyi moto, mvua ya mawe na theluji, upepo wa tufani unaotimiza amri yake! Msifuni enyi milima na vilima, miti ya matunda na misitu! Msifuni enyi wanyama wa porini na wafugwao, viumbe vitambaavyo na ndege wote! Msifuni enyi wafalme na mataifa yote; viongozi na watawala wote duniani! Msifuni enyi wavulana na wasichana; wazee wote na watoto pia! Nyote lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu, maana jina lake peke yake latukuka; utukufu wake wapita dunia na mbingu. Amewapa watu wake nguvu; heshima kwa watu wote waaminifu, watu wa Israeli wapenzi wake. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya; msifuni katika kusanyiko la waaminifu! Furahi ee Israeli kwa sababu ya Muumba wako, wakazi wa Siyoni shangilieni kwa sababu ya Mfalme wenu. Lisifuni jina lake kwa ngoma, mwimbieni kwa ngoma na zeze. Maana Mwenyezi-Mungu hupendezwa na watu wake; yeye huwapamba wanyonge kwa ushindi. Watu waaminifu wafurahi kwa fahari; washangilie hata walalapo. Wabubujike sifa kuu za Mungu, na panga zenye makali kuwili mikononi mwao, wawalipe kisasi watu wa mataifa, wawaadhibu watu wasiomjua Mungu; wawafunge wafalme wao kwa minyororo, na viongozi wao kwa pingu za chuma, kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa! Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mungu katika patakatifu pake; msifuni katika mbingu zake kuu. Msifuni kwa sababu ya matendo yake makuu; msifuni kwa ajili ya utukufu wake mkuu. Msifuni kwa mlio wa tarumbeta; msifuni kwa zeze na kinubi! Msifuni kwa ngoma na kucheza; msifuni kwa filimbi na banjo! Msifuni kwa kupiga matoazi. Msifuni kwa matoazi ya sauti kubwa. Kila kiumbe hai kimsifu Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Hizi ni methali za Solomoni mfalme wa Israeli, mwana wa Daudi. Methali hizi zawapatia watu hekima na nidhamu; zawafanya waelewe maneno ya busara, zawafanya kuwa na nidhamu, utaratibu, uadilifu, haki na kutenda kwa usawa. Huwapatia wajinga werevu na vijana maarifa na hadhari. Mwenye hekima azisikie na kuongeza elimu yake, naye mwenye busara apate mwongozo. Mtu aelewe methali na mifano, maneno ya wenye hekima na vitendawili vyao. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa maarifa, lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu. Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako, wala usiyapuuze mafundisho ya mama yako; hayo yatakupamba kilemba kichwani pako, kama mkufu shingoni mwako. Mwanangu, usikubali kushawishiwa na wenye dhambi. Wakisema: “Twende tukamvizie mtu na kumuua; njoo tukawashambulie wasio na hatia! Tutawameza kama Kuzimu wakiwa hai, watakuwa kama wale washukao Shimoni. Tutajitwalia mali zote za thamani, nyumba zetu tutazijaza nyara. Njoo ushirikiane nasi, vyote tutakavyopata tutagawana.” Wewe mwanangu usiandamane nao, uzuie mguu wako usifuatane nao. Maana wao wako mbioni kutenda maovu, haraka zao zote ni za kumwaga damu. Mtego utegwao huku ndege anaona, mtego huo wategwa bure. Wao huvizia na kujiangamiza wao wenyewe, hutega mtego wa kujinasa wao wenyewe. Ndivyo zilivyo njia za waishio kwa ukatili; ukatili huyaangamiza maisha ya wakatili. Hekima huita kwa sauti barabarani, hupaza sauti yake sokoni; huita juu ya kuta, hutangaza penye malango ya mji: “Enyi wajinga! Mpaka lini mtapenda kuwa wajinga? Mpaka lini wenye dharau watafurahia dharau zao, na wapumbavu kuchukia maarifa? Sikilizeni maonyo yangu; nitawamiminia mawazo yangu, nitawajulisha maneno yangu. Kwa kuwa nimewaita mkakataa kusikiliza, nimewapungia mkono mje mkakataa, mkapuuza mashauri yangu yote, wala hamkuyajali maonyo yangu, nami pia nitayachekelea maafa yenu, nitawadhihaki mnapokumbwa na hofu, hofu itakapowakumba kama tufani, maafa yenu yatakapowavamia kama kimbunga, wakati udhia na dhiki vitakapowapata. Hapo ndipo mtakaponiita lakini sitaitika; mtanitafuta kwa bidii lakini hamtanipata. Kwa kuwa mliyachukia maarifa, wala hamkuchagua kumcha Mwenyezi-Mungu; maadamu mlikataa shauri langu, mkayapuuza maonyo yangu yote; basi, mtakula matunda ya mienendo yenu, mtavimbiwa kwa hila zenu wenyewe. Maana wajinga hujiua kwa ukaidi wao, wapumbavu hujiangamiza kwa kujiamini kwao. Lakini kila anisikilizaye atakaa salama, atatulia bila kuogopa mabaya.” Mwanangu, ukiyakubali maneno yangu, na kuyathamini maagizo yangu; ukitega sikio lako kusikiliza hekima, na kuuelekeza moyo wako upate ufahamu; naam, ukiomba upewe busara, ukisihi upewe ufahamu; ukiitafuta hekima kama fedha, na kuitaka kama hazina iliyofichika; hapo utaelewa ni nini kumcha Mwenyezi-Mungu, utafahamu maana ya kumjua Mungu. Maana Mwenyezi-Mungu huwapa watu hekima; kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu. Huwawekea wanyofu akiba ya hekima safi, yeye ni ngao kwa watu waishio kwa uaminifu. Huilinda mienendo ya watu watendao haki, na kuzihifadhi njia za waaminifu wake. Ukinisikiliza utafahamu uadilifu na haki, utajua jambo lililo sawa na jema. Maana hekima itaingia moyoni mwako, na maarifa yataipendeza nafsi yako. Busara itakulinda, ufahamu utakuhifadhi; vitakuepusha na njia ya uovu, na watu wa maneno mapotovu; watu waziachao njia nyofu, ili kuziendea njia za giza; watu wafurahiao kutenda maovu, na kupendezwa na upotovu wa maovu; watu ambao mienendo yao imepotoka, nazo njia zao haziaminiki. Hekima itakuwezesha kumkwepa mwanamke mwasherati, mwanamke malaya wa maneno matamu; mwanamke amwachaye mwenzi wa ujana wake, na kulisahau agano la Mungu wake. Nyumba yake yaelekea kuzimu, njia zake zinakwenda ahera. Yeyote amwendeaye kamwe harudi, wala hairudii tena njia ya uhai. Kwa hiyo utafuata mfano wa watu wema, na kuzingatia mienendo ya waadilifu. Maana wanyofu wataipata nchi, na waaminifu watadumu ndani yake. Lakini waovu wataondolewa nchini, na wenye hila watangolewa humo. Mwanangu, usiyasahau mafundisho yangu, bali kwa moyo wako uzishike amri zangu. Maana yatakupa wingi wa siku, maisha marefu na fanaka kwa wingi. Utii na uaminifu visitengane nawe. Vifunge shingoni mwako; viandike moyoni mwako. Hivyo utakubalika na kusifika, mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu. Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako. Usijione wewe mwenyewe kuwa mwenye hekima; mche Mwenyezi-Mungu na kujiepusha na uovu. Hiyo itakuwa dawa mwilini mwako, na kiburudisho mifupani mwako. Mheshimu Mwenyezi-Mungu kwa mali yako, na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Hapo ghala zako zitajaa nafaka, na mapipa yako yatafurika divai mpya. Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi-Mungu, wala usiudhike kwa maonyo yake; maana Mwenyezi-Mungu humwonya yule ampendaye, kama baba amwonyavyo mwanawe mpenzi. Heri mtu anayegundua hekima, mtu yule anayepata ufahamu. Hekima ni bora kuliko fedha, ina faida kuliko dhahabu. Hekima ina thamani kuliko johari, hamna unachotamani kiwezacho kulingana nayo. Kwa mkono wake wa kulia Hekima atakupa maisha marefu; kwa mkono wake wa kushoto atakupa mali na heshima. Njia zake ni za kupendeza, zote zaelekea kwenye amani. Hekima ni mti wa uhai kwa wote wampatao; wana heri wote wanaoshikamana naye. Kwa hekima Mwenyezi-Mungu aliweka misingi ya dunia, kwa akili aliziimarisha mbingu. Kwa maarifa yake vilindi vilipasuka, na mawingu yakadondosha umande. Mwanangu, zingatia hekima safi na busara; usiviache vitoweke machoni pako, navyo vitakuwa uhai nafsini mwako, na pambo zuri shingoni mwako. Hapo utaweza kwenda zako kwa usalama, wala mguu wako hautajikwaa. Ukiketi hutakuwa na hofu; ukilala utapata usingizi mtamu. Usiogope juu ya tishio la ghafla, wala shambulio kutoka kwa waovu, Maana Mwenyezi-Mungu ndiye atakayekutegemeza; atakuepusha usije ukanaswa mtegoni. Usimnyime mtu anayehitaji msaada, ikiwa unao uwezo wa kufanya hivyo. Usimwambie jirani yako aende zake hadi kesho, hali wewe waweza kumpa anachohitaji leo. Usipange maovu dhidi ya jirani yako, anayeishi karibu nawe bila wasiwasi. Usigombane na mtu bila sababu ikiwa hajakudhuru kwa lolote. Usimwonee wivu mtu mkatili, wala usiige mwenendo wake. Maana waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; lakini yeye huwafanya marafiki zake wale walio wanyofu. Mwenyezi-Mungu huapiza nyumba za waovu, lakini huyabariki makao ya waadilifu. Yeye huwadharau wenye dharau, lakini huwafadhili wanyenyekevu. Wenye hekima watavuna heshima, lakini wapumbavu watapata fedheha. Wanangu, sikilizeni mwongozo wa baba yenu, tegeni sikio mpate kuwa na akili. Maana ninawapa maagizo mema, msiyakatae mafundisho yangu. Mimi pia nilikuwa mtoto mwenye baba, nilikuwa mpole, kipenzi cha mama yangu. Baba yangu alinifundisha hiki: “Zingatia kwa moyo maneno yangu, shika amri zangu nawe utaishi. Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usisahau wala kupuuza maneno yangu. Usimwache Hekima, naye atakutunza; umpende, naye atakulinda. Jambo la msingi ni kujipatia hekima; toa vyote ulivyonavyo ujipatie akili. Mthamini sana Hekima, naye atakutukuza; ukimshikilia atakupa heshima. Atakuvika kilemba kizuri kichwani pako, atakupa taji maridadi.” Mwanangu, sikia na kuyapokea maneno yangu, ili upate kuwa na miaka mingi ya kuishi. Nimekufundisha njia ya hekima, nimekuongoza katika njia nyofu. Ukitembea hatua zako hazitazuiwa, wala ukikimbia hutajikwaa. Zingatia mafundisho ya Hekima na usimwache aponyoke, mshike kwa makini maana yeye ni uhai wako. Usijiingize katika njia ya waovu, wala usifuate mwenendo wa watu wabaya. Iepe njia hiyo wala usiikaribie; jiepushe nayo, uende zako. Waovu kamwe hawalali wasipotenda uovu; hawapati usingizi wasipomkwaza mtu. Maana uovu ndicho chakula chao, ukatili ndiyo divai yao. Njia ya watu wema ni kama nuru ya alfajiri, ambayo hungaa zaidi na zaidi hata mchana kamili. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene, hawajui kinachowafanya wajikwae. Mwanangu, sikiliza kwa makini maneno yangu, itegee sikio misemo yangu. Usiyaache yatoweke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako. Maana hayo ni uhai kwa mtu anayeyapata, ni dawa kwa mwili wake wote. Linda moyo wako kwa uangalifu wote, maana humo zatoka chemchemi za uhai. Tenga mbali nawe lugha potovu; wala midomo yako isitamke maneno madanganyifu. Uyaelekeze macho yako mbele kwa ujasiri, mtazamo wako uwe mbele moja kwa moja. Fikiria njia utakayochukua, na hatua zako zote zitakuwa kamili. Usigeukie kulia wala kushoto; epusha mguu wako mbali na uovu. Mwanangu, sikia hekima yangu, tega sikio usikilize elimu yangu. Ndipo utakapoweza kuhifadhi busara, na midomo yako izingatie maarifa. Mdomo wa mwanamke mpotovu ni mtamu kama asali, maneno yake ni laini kuliko mafuta; lakini hatimaye ni mchungu kama pakanga, ni mkali kama upanga wenye makali kuwili. Nyayo zake zaelekea chini mautini, hatua zake zaenda kuzimu. Yeye haijali njia ya uhai, njia zake ni za kutangatanga, wala hajui. Sasa enyi wanangu, nisikilizeni, wala msisahau maneno ya kinywa changu. Iepushe njia yako mbali naye, wala usiukaribie mlango wa nyumba yake. Usije ukawapa wengine heshima yako, na wakatili miaka yako; wageni wasije wakajishibisha kwa mali yako, na jasho lako likaishia nyumbani kwa mgeni. Mwishoni mwa maisha yako utaomboleza wakati mwili wako utakapoangamizwa. Hapo utasema, “Jinsi gani nilivyochukia nidhamu, na kudharau maonyo moyoni mwangu! Sikuisikiliza sauti ya waalimu wangu, wala kuwategea sikio wakufunzi wangu. Sasa niko karibu kuangamia kabisa mbali na jumuiya ya watu.” Mkeo ni kama kisima cha maji safi: Kunywa maji ya kisima chako mwenyewe. Ya nini chemchemi zako zitawanywe mbali, na vijito vya maji barabarani? Hiyo ni yako wewe mwenyewe, wala usiwashirikishe watu wengine. Chemchemi yako na ibarikiwe, umfurahie mke uliyemwoa ukiwa kijana. Ni mzuri kama ayala, apendeza kama paa. Mahaba yake yakufurahishe kila wakati, umezwe daima na pendo lake. Mwanangu, ya nini kutekwa na mwanamke mwasherati? Ya nini kumkumbatia kifuani mwanamke mgeni? Kumbuka njia za mtu zi wazi mbele ya Mwenyezi-Mungu; yeye anaona kila hatua anayochukua binadamu. Mtu mwovu hunaswa kwa uovu wake mwenyewe; hukamatwa katika tanzi za dhambi yake mwenyewe. Yeye hufa kwa utovu wa nidhamu, huangamia kwa sababu ya upuuzi wake mkuu. Mwanangu, kama umejitolea kumdhamini jirani yako, ikiwa umetoa ahadi yako kwa ajili ya mtu huyo, umejibana kwa maneno yako mwenyewe, umejinasa kwa ahadi uliyofanya. Ujue kwamba uko chini ya mamlaka ya mwenzio, lakini mwanangu, ukitaka kujiokoa, basi fanya hivi: Mwendee mtu huyo mara moja umsihi akupe uhuru wako. Jitahidi usiache macho yako yapate usingizi, wala kope za macho yako zisinzie. Jiokoe kwa kujitoa katika mtego huo, mithili ya paa ama ndege amtorokavyo mwindaji. Ewe mvivu! Hebu ukamchungulie sisimizi, fikiria namna yake ya kuishi ukapate hekima. Sisimizi hana kiongozi, ofisa, wala mtawala; lakini hujiwekea chakula wakati wa kiangazi, hujikusanyia akiba wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hapo mpaka lini? Utaamka lini katika usingizi wako? Wasema: “Acha nilale kidogo tu, acha nisinzie kidogo! Niache nikunje mikono nipumzike kidogo!” Wakati huo umaskini utakuvamia kama mnyanganyi, ufukara utakufuata kama jambazi. Mtu mwovu, mtu asiyefaa kitu, huzururazurura akisema maneno mapotovu. Hukonyeza jicho kuwakosesha wengine, huparuza kwa nyayo, na kuashiria watu kwa vidole. Akiwa amejaa ulaghai moyoni hutunga maovu, huzusha ugomvi kila mahali. Kutokana na hayo maafa yatamvamia ghafla, ghafla atadhurika vibaya asiweze kupona tena. Kuna vitu sita anavyochukia Mwenyezi-Mungu; naam, vitu saba ambavyo ni chukizo kwake: Macho ya kiburi, ulimi mdanganyifu, mikono inayoua wasio na hatia, moyo unaopanga mipango miovu, miguu iliyo mbioni kutenda maovu, shahidi wa uongo abubujikaye uongo, na mtu achocheaye fitina kati ya ndugu. Mwanangu, shika maagizo ya baba yako, wala usisahau mafundisho ya mama yako; yaweke daima moyoni mwako, yafunge shingoni mwako. Yatakuongoza njiani mwako, yatakulinda wakati ulalapo, yatakushauri uwapo macho mchana. Maana amri hiyo ni taa, na sheria hiyo ni mwanga. Maonyo hayo na nidhamu yatuweka njiani mwa uhai. Yatakulinda mbali na mwanamke mbaya, yatakuepusha na maneno matamu ya mwanamke mgeni. Usimtamani mwanamke huyo kwa uzuri wake, wala usikubali kunaswa kwa kope za macho yake. Mtu hupoteza kipande cha mkate kwa malaya, lakini kwa mke wa mtu mwingine utapoteza uhai wako wote. Je, waweza kuweka moto kifuani na nguo zako zisiungue? Je, waweza kukanyaga makaa ya moto na nyayo zako zisiungue? Ndivyo alivyo mwanamume alalaye na mke wa mwenzake; yeyote anayemgusa mwanamke huyo hataacha kuadhibiwa. Watu hawambezi sana mtu akiiba kwa sababu ya njaa; lakini akipatikana lazima alipe mara saba; tena atatoa mali yote aliyo nayo. Mwanamume anayezini na mke wa mtu hana akili kabisa; huyo hujiangamiza yeye mwenyewe. Atapata majeraha na madharau; fedheha atakayopata haitamtoka. Maana wivu wa mume humfanya kuwa mkali kabisa; wakati atakapolipiza kisasi hana cha kuhurumia. Hatakubali fidia yoyote; wala kutulizwa na zawadi zako nyingi. Mwanangu, yashike maneno yangu, zihifadhi kwako amri zangu. Zifuate amri zangu nawe utaishi; yalinde mafundisho yangu kama mboni ya jicho lako. Yafunge vidoleni mwako; yaandike moyoni mwako. Iambie Hekima: “Wewe ni dada yangu”, na Busara “Wewe ni rafiki yangu”. Vitakulinda mbali na mwanamke mbaya, vitakuepusha na maneno matamu ya mwanamke mgeni. Siku moja dirishani mwa nyumba yangu, nilichungulia nje kupitia viunzi vya dirisha, nikawaona vijana wengi wajinga, na mmoja hasa aliyekuwa mpumbavu. Huyo alikuwa akitembea kwenye barabara ile, karibu na kona alikoishi mwanamke fulani. Basi akashika njia iendayo nyumbani kwa mwanamke huyo. Ilikuwa yapata wakati wa jioni, giza na usiku vilikuwa vimeanza kuingia. Punde kijana akakutana na huyo mwanamke; amevalia kama malaya, ana mipango yake. Alikuwa mwanamke wa makelele na mkaidi; miguu yake haitulii nyumbani: Mara barabarani, mara sokoni, katika kila kona ya njia hakosekani akivizia. Alimkumbatia kijana huyo na kumbusu, na kwa maneno matamu, akamwambia: “Ilinilazimu kutoa tambiko zangu; leo hii nimekamilisha nadhiri yangu. Ndio maana nimetoka ili nikulaki, nimekutafuta kwa hamu nikakupata. Nimetandika kitanda changu vizuri, kwa shuka za rangi za kitani kutoka Misri. Nimekitia manukato, manemane, udi na mdalasini. Njoo tulale pamoja mpaka asubuhi; njoo tujifurahishe kwa mahaba. Mume wangu hayumo nyumbani, amekwenda safari ya mbali. Amechukua bunda la fedha; hatarejea nyumbani karibuni.” Alimshawishi kwa maneno mengi ya kubembeleza; kijana akashawishika kwa maneno yake matamu. Hapo akamfuata huyo mwanamke moja kwa moja, kama ng'ombe aendaye machinjioni, kama paa arukiaye mtegoni. Hakutambua kwamba hiyo itamgharimu maisha yake, mpaka alipojikuta amekuwa kama amechomwa mshale moyoni, amekuwa kama ndege aliyenaswa wavuni. Sasa wanangu, nisikilizeni; yategeeni sikio maneno ya kinywa changu. Msikubali kuongozwa na mwanamke kama huyo, wala msipitepite katika mapito yake. Maana amewaangusha wanaume wengi; ni wengi mno hao aliowachinja. Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, ni mahali pa kuteremkia mautini. Sikilizeni! Hekima anaita! Busara anapaza sauti yake! Juu penye mwinuko karibu na njia, katika njia panda ndipo alipojiweka. Karibu na malango ya kuingilia mjini, mahali wanapoingia watu anaita kwa sauti: “Enyi watu wote, nawaita nyinyi! Wito wangu ni kwa ajili ya binadamu. Enyi wajinga, jifunzeni kuwa na akili; sikilizeni kwa makini enyi wapumbavu. Sikilizeni maana nitakachosema ni jambo muhimu; midomoni mwangu mtatoka mambo ya adili. Kinywa changu kitatamka kweli tupu; uovu ni chukizo midomoni mwangu. Kinywa changu kitatamka maneno ya kweli, udanganyifu ni haramu midomoni mwangu. Kwa mtu mwelewa kila kitu ni wazi, kwa mwenye maarifa yote ni sawa. Chagua mafundisho yangu badala ya fedha; na maarifa badala ya dhahabu safi. “Mimi Hekima nina thamani kuliko johari; chochote unachotamani hakiwezi kulingana nami. Mimi Hekima ninao ujuzi; ninayo maarifa na busara. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni kuchukia uovu. Nachukia kiburi, majivuno na maisha mabaya; nachukia na lugha mbaya. Nina uwezo wa kushauri na nina hekima. Ninao ujuzi na nina nguvu. Kwa msaada wangu wafalme hutawala, watawala huamua yaliyo ya haki. Kwa msaada wangu viongozi hutawala, wakuu na watawala halali. Nawapenda wale wanaonipenda; wanaonitafuta kwa bidii hunipata. Utajiri na heshima viko kwangu, mali ya kudumu na fanaka. Matunda yangu ni mazuri kuliko dhahabu safi, faida yangu yashinda ile ya fedha bora. Natembea katika njia ya uadilifu; ninafuata njia za haki. Mimi huwatajirisha wanaonipenda, huzijaza tele hazina zao wanipendao. “Mwenyezi-Mungu aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, zama za zama kabla ya kuwako kitu chochote. Nilifanywa mwanzoni mwa nyakati, nilikuwako kabla ya dunia kuanza. Nilizaliwa kabla ya vilindi vya bahari, kabla ya chemchemi zibubujikazo maji. Kabla ya milima haijaumbwa, na vilima kusimamishwa mahali pake, mimi nilikuwako tayari. Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake, wala chembe za kwanza za mavumbi ya dunia. Nilikuwako wakati alipoziweka mbingu, wakati alipopiga duara juu ya bahari; wakati alipoimarisha mawingu mbinguni, alipozifanya imara chemchemi za bahari; wakati alipoiwekea bahari mpaka wake, maji yake yasije yakavunja amri yake; wakati alipoiweka misingi ya dunia. Nilikuwa pamoja naye kama fundi stadi, nilikuwa furaha yake kila siku, nikishangilia mbele yake daima, nikifurahia dunia na wakazi wake, na kupendezwa kuwa pamoja na wanadamu. “Sasa basi wanangu, nisikilizeni: Heri wale wanaofuata njia zangu. Sikilizeni mafunzo mpate hekima, wala msiyakatae. Heri mtu anayenisikiliza, anayekaa kila siku mlangoni pangu, anayekesha karibu na milango yangu. Anayenipata mimi amepata uhai, amepata upendeleo kwa Mwenyezi-Mungu. Asiyenipata anajidhuru mwenyewe; wote wanaonichukia wanapenda kifo.” Hekima amejenga nyumba yake, nyumba yenye nguzo saba. Amechinja wanyama wa karamu, divai yake ameitayarisha, ametandika meza yake. Amewatuma watumishi wake wa kike mjini, waite watu kutoka kwenye vilele vya miinuko: “Yeyote aliye mjinga na aje hapa!” Na yeyote aliye mpumbavu humwambia: “Njoo ukale chakula, na unywe divai niliyotengeneza. Achana na ujinga upate kuishi; fuata njia ya akili.” Anayemkosoa mwenye dharau hupata matusi, amkaripiaye mwovu huishia kwa kuumizwa. Usimwonye mwenye dharau maana atakuchukia; mwonye mwenye hekima naye atakupenda. Mfunze mwenye hekima naye atazidi kuwa na hekima; mfundishe mwadilifu naye atazidi kuelimika. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa hekima; na kumjua yule Mtakatifu ni kupata akili. Kwa msaada wangu mimi Hekima siku zako zitaongezwa; utaongezewa miaka mingi maishani mwako. Kama una hekima, itakufaa wewe mwenyewe; kama ukiidharau, mwenyewe utapata hasara. Mwanamke mpumbavu ana kelele, hajui kitu wala hana haya. Hukaa kitako mlangoni mwa nyumba yake, huweka kiti chake mahali pa juu mjini, na kuwaita watu wapitao njiani, watu wanaokwenda kwenye shughuli zao: “Yeyote aliye mjinga na aje hapa!” Na yeyote aliye mpumbavu humwambia: “Maji ya wizi ni matamu sana; mkate unaoliwa kwa siri ni mzuri sana.” Lakini mjinga hajui kwamba humo mna wafu, wageni wa mwanamke huyo wamo chini Kuzimu. Hizi ni methali za Solomoni: Mtoto mwenye hekima ni furaha ya baba yake; lakini mtoto mpumbavu ni huzuni ya mama yake. Mali iliyopatikana kwa njia mbaya haifai, lakini uadilifu huokoa mtu kutoka kifoni. Mwenyezi-Mungu hawaachi waadilifu wapate njaa, lakini huzipinga tamaa za waovu. Uvivu husababisha umaskini, lakini mkono wa mtu wa bidii hutajirisha. Mwenye busara hukusanya wakati wa mavuno, kulala wakati wa kuvuna ni aibu. Mwadilifu hujiletea baraka yeye mwenyewe, lakini kinywa cha mwovu kimesongwa na ukatili. Waadilifu hukumbukwa kwa baraka, lakini waovu watasahaulika kabisa. Mwenye hekima moyoni hutii amri, lakini mpumbavu aropokaye ataangamia. Aishiye kwa unyofu huishi salama, apotoshaye maisha yake atagunduliwa. Akonyezaye kwa nia mbaya huzusha taabu, lakini aonyaye kwa ujasiri huleta amani. Kinywa cha mwadilifu ni chemchemi ya uhai, lakini kinywa cha mwovu kimesongwa na ukatili. Chuki huzusha ugomvi, lakini upendo hufunika makosa yote. Kinywani mwa mwenye ufahamu mna hekima, lakini wasio na akili watachapwa viboko mgongoni. Wenye hekima huhifadhi maarifa, lakini kuropoka kwa mpumbavu huleta maangamizi haraka. Mali ya tajiri ndio ngome yake, umaskini wa maskini humletea maangamizi. Tuzo la mtu mwema ni uhai, lakini mwovu huishia katika dhambi. Anayekubali maonyo anaelekea kwenye uhai, lakini anayekataa kuonywa amepotoka. Amchukiaye mwingine kwa siri ni mnafiki, anayemsingizia mtu ni mpumbavu. Penye maneno mengi hapakosekani makosa, lakini aneyeuzuia ulimi wake ana busara. Maneno ya mwadilifu ni kama fedha bora; akili ya mtu mwovu haina thamani yoyote. Maneno ya mwadilifu huwafaa watu wengi, lakini wapumbavu hufa kwa kukosa akili. Baraka za Mwenyezi-Mungu ndizo ziletazo fanaka, juhudi za mtu haziongezi hapo chochote. Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo; lakini watu wenye busara hufurahia hekima. Anachoogopa mtu mwovu ndicho kitakachompata, lakini anachotamani mwadilifu ndicho atakachopewa. Kimbunga hupita na mwovu hutoweka, lakini mwadilifu huimarishwa milele. Kama ilivyo siki kwa meno au moshi machoni, ndivyo alivyo mvivu kwa bwana wake. Kumcha Mwenyezi-Mungu hurefusha maisha, lakini miaka ya waovu itakuwa mifupi. Tumaini la mwadilifu huishia kwenye furaha, lakini tazamio la mwovu huishia patupu. Mwenyezi-Mungu ni ngome ya wanyofu, lakini watendao maovu atawaangamiza. Waadilifu kamwe hawataondolewa nchini, lakini waovu hawatakaa katika nchi. Kinywa cha mwadilifu hutoa mambo ya hekima, lakini ulimi wa mtu mbaya utakatiliwa mbali. Midomo ya waadilifu hujua yanayokubalika, lakini vinywa vya waovu husema tu maovu. Mizani ya udanganyifu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, lakini matumizi ya kipimo halali ni furaha kwake. Kiburi huandamana na fedheha, lakini kwa watu wanyenyekevu mna hekima. Unyofu wa watu wema huwaongoza, upotovu wa wenye hila huwaangamiza. Utajiri haufai kitu siku ya ghadhabu, lakini uadilifu huokoa kutoka kifo. Uadilifu wa watu wanyofu huinyosha njia yao, lakini waovu huanguka kwa uovu wao wenyewe. Uadilifu wa wanyofu huwaokoa na hatari, lakini wafitini hunaswa kwa tamaa zao wenyewe. Mwovu akifa tumaini lake nalo hutoweka; tazamio la asiyemcha Mungu huishia patupu. Mtu mnyofu huokolewa katika shida, na mwovu huingia humo badala yake. Asiyemcha Mungu huangamiza wengine kwa mdomo wake, lakini mwadilifu huokolewa kwa maarifa yake. Waadilifu wakipata fanaka mji hushangilia, na waovu wakiangamia watu hupiga vigelegele. Mji hufanikishwa kwa baraka za wanyofu, lakini huangamizwa kwa mdomo wa waovu. Anayemdharau jirani yake hana akili, mtu mwenye busara hukaa kimya. Apitapitaye akichongea hutoa siri, lakini anayeaminika rohoni huficha siri. Pasipo na uongozi taifa huanguka, penye washauri wengi pana usalama. Anayemdhamini mgeni atakuja juta, lakini anayechukia mambo ya dhamana yu salama. Mwanamke mwema huheshimiwa, mwanamume mwenye bidii hutajirika. Mtu mkarimu hufaidika yeye mwenyewe, lakini mtu mkatili hujiumiza mwenyewe. Faida anayopata mwovu ni ya uongo, lakini atendaye mema hakika atapata faida ya kweli. Mtu anayepania kuwa mwadilifu ataishi, lakini anayechagua kutenda maovu atakufa. Wenye nia mbaya ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, lakini wenye mwenendo mwema ni furaha yake. Hakika mwovu hataepa kuadhibiwa, lakini waadilifu wataokolewa. Mwanamke mzuri asiye na akili, ni kama pete ya dhahabu puani mwa nguruwe. Matazamio ya waadilifu yana matokeo mema; tamaa za waovu huishia katika ghadhabu. Atoaye kwa ukarimu huzidi kutajirika; lakini bahili huzidi kudidimia katika umaskini. Mtu mkarimu atafanikishwa, amnyweshaye mwingine maji naye atanyweshwa. Watu humlaani afichaye nafaka, lakini humtakia baraka mwenye kuiuza. Atafutaye kutenda mema hupata fadhili, lakini atafutaye kutenda maovu atapatwa na maovu. Anayetegemea mali zake ataanguka, lakini mwadilifu atastawi kama jani bichi. Anayeivunja nyumba yake ataambua upepo. Mpumbavu atakuwa mtumwa wa wenye hekima. Matendo ya mwadilifu huleta uhai, lakini uhalifu huuondoa uhai. Ikiwa mwadilifu hupata tuzo hapa duniani, hakika mwovu na mwenye dhambi atapatilizwa. Apendaye nidhamu hupenda maarifa, bali asiyependa kuonywa ni mjinga. Mtu mwema hufadhiliwa na Mwenyezi-Mungu, lakini mwenye nia mbaya hulaaniwa na Mungu. Mtu hawi imara kwa kutenda maovu, lakini hakuna kiwezacho kumngoa mtu mwadilifu. Mke mwema ni taji ya fahari kwa mumewe; amwaibishaye mumewe ni kama kidonda mifupani mwake. Mawazo ya mwadilifu ni ya haki; mashauri ya mwovu ni ya udanganyifu. Maneno ya waovu lengo lake ni kuua, lakini maneno ya waadilifu huwaokoa wanaotishwa. Waovu huangamizwa na kutoweka kabisa, lakini jamaa ya waadilifu hudumishwa. Mtu husifiwa kadiri ya hekima yake, lakini mtu wa fikira mbaya hudharauliwa. Afadhali mtu wa chini anayejitegemea, kuliko ajitakiaye makuu na kukosa chakula. Mtu mwadilifu huwajali wanyama wake, lakini huruma ya mwovu ni ukatili. Mkulima mwenye bidii ana chakula tele, lakini afuataye mambo yasiyofaa hana akili. Waovu hutamani faida isiyo halali, lakini mtu mwadilifu husimama imara. Mtu mwovu hunaswa kwa uongo wake mwenyewe, lakini mwadilifu hutoka katika taabu. Mtu hufanikiwa kutokana na maneno yake kama apatavyo matokeo ya kazi za mikono yake. Mpumbavu huiona njia yake kuwa sawa, lakini mwenye hekima husikiliza shauri. Udhia wa mpumbavu hujulikana mara, lakini mwerevu huyapuuza matukano. Msema kweli hutoa ushahidi wa kweli, lakini shahidi wa uongo hutamka udanganyifu. Maneno ya ovyo hujeruhi kama upanga, lakini asemayo mwenye hekima huponesha kidonda. Ukweli hudumu milele, lakini uongo ni wa kitambo tu. Wanaopanga maovu wamejaa udanganyifu moyoni, lakini wanaonuia mema hupata furaha. Waadilifu hawapatwi na jambo lolote baya, lakini waovu wamejaa dhiki. Midomo isemayo uongo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, lakini watu waaminifu ni furaha yake. Mwenye busara huficha maarifa yake, lakini wapumbavu hutangaza upumbavu wao. Kuwa na bidii kutampa mtu cheo, lakini uvivu utamfanya mtumwa. Wasiwasi moyoni humkosesha mtu raha, lakini neno jema humchangamsha. Mtu mwadilifu huuepa uovu, lakini njia ya waovu huwapotosha wenyewe. Mwindaji mvivu hatapata anachowinda, lakini mwenye bidii atafanikiwa. Uadilifu ni njia ya uhai, lakini uovu huongoza katika mauti. Mtoto mwenye hekima husikia maagizo ya baba yake, lakini mwenye dharau hasikilizi maonyo. Mtu mwema hupata mema kutokana na maneno yake, lakini wadanganyifu huishi kwa ukatili. Achungaye mdomo wake huyahifadhi maisha yake, anayeropoka ovyo hujiletea maangamizi. Mvivu hutamani lakini hapati chochote, hali mwenye bidii hujaliwa riziki kwa wingi. Mwadilifu huuchukia uongo, lakini mwovu hutenda kwa aibu na fedheha. Uadilifu huwalinda wenye mwenendo mnyofu, lakini dhambi huwaangusha waovu. Baadhi hujidai kuwa matajiri kumbe hawana kitu; wengine hujiona kuwa maskini hali wana mali tele. Fidia ya mtu ni mali yake, lakini maskini hana cha kutishwa. Mwadilifu hungaa kama taa iwakayo vizuri, lakini waovu ni kama taa inayozimika. Kiburi husababisha tu ugomvi, lakini kwa wanaokubali shauri jema mna hekima. Mali ya harakaharaka hutoweka, lakini akusanyaye kidogokidogo ataiongeza. Tumaini la kungojangoja huumiza moyo, lakini tazamio linalotimia ni mti wa uhai. Anayedharau mawaidha anajiletea maangamizi, lakini anayetii amri atapewa tuzo. Mafundisho ya wenye hekima ni chemchemi ya uhai; humwezesha mtu kuiepa mitego ya kifo. Kuwa na akili huleta fadhili, lakini njia ya waovu ni ya taabu Mwenye busara hutenda kila kitu kwa akili, lakini mpumbavu hutembeza upumbavu wake. Mjumbe mbaya huwatumbukiza watu taabuni, lakini mjumbe mwaminifu huleta nafuu. Umaskini na fedheha humpata asiyejali mafundisho, lakini mwenye kusikia maonyo huheshimiwa. Inafurahisha upatapo kile unachotaka, kwa hiyo wapumbavu huchukia kuepa uovu. Anayeandamana na wenye hekima hupata hekima, lakini anayejiunga na wapumbavu atapata madhara. Watendao dhambi huandamwa na balaa, lakini waadilifu watatuzwa mema. Mtu mwema huwaachia urithi uzao wake, lakini mali ya mwenye dhambi imerundikiwa waadilifu. Shamba la maskini hutoa mazao mengi, lakini bila haki hunyakuliwa. Asiyemwadhibu mtoto wake hampendi; lakini ampendaye mwanawe humrudi mapema. Mwadilifu anacho chakula cha kumtosheleza, lakini tumbo la waovu hutaabika kwa njaa. Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake, lakini mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe. Mwenye mwenendo mnyofu humcha Mwenyezi-Mungu, lakini mpotovu humdharau Mungu. Mpumbavu hujiadhibu mwenyewe kwa kuropoka kwake, lakini mwenye hekima hulindwa na maneno yake. Bila ng'ombe wa kulima ghala za mtu ni tupu, mavuno mengi hupatikana kwa nguvu ya ng'ombe wa kulima. Shahidi mwaminifu hasemi uongo, lakini asiyeaminika hububujika uongo. Mwenye dharau hutafuta hekima bure, lakini mwenye busara hupata maarifa kwa urahisi. Ondoka mahali alipo mpumbavu, maana hapo alipo hamna maneno ya hekima. Hekima ya mwenye busara humwonesha njia yake, lakini upumbavu wa wapumbavu huwadanganya wenyewe. Wapumbavu huchekelea dhambi, bali wanyofu hupata fadhili kwa Mungu. Moyo waujua uchungu wake wenyewe, wala mgeni hawezi kushiriki furaha yake. Nyumba ya mtu mwovu itabomolewa, lakini hema ya wanyofu itaimarishwa. Njia unayodhani kuwa ni sawa, mwishoni yaweza kukuongoza kwenye kifo. Huzuni yaweza kufichika katika kicheko; baada ya furaha huja majonzi. Mtu mpotovu atavuna matunda ya mwenendo wake, naye mtu mwema atapata tuzo la matendo yake. Mjinga huamini kila kitu anachoambiwa, lakini mwenye busara huwa na tahadhari. Mwenye hekima ni mwangalifu na huepa uovu, lakini mpumbavu hajizuii wala hana uangalifu. Mwenye kuwaka hasira haraka hutenda kipumbavu, lakini mwenye busara ana uvumilivu. Wajinga hurithi upumbavu, lakini wenye busara hutuzwa taji ya maarifa. Waovu watapiga magoti mbele ya watu wema, watu wabaya mlangoni mwa waadilifu. Maskini huchukiwa hata na jirani yake, lakini tajiri ana marafiki wengi. Anayemdharau jirani yake ni mwenye dhambi, bali ana heri aliye mwema kwa maskini. Anayepanga maovu kweli anakosea! Wanaopanga kutenda mema hufadhiliwa. Bidii katika kila kazi huleta faida, lakini maneno matupu huleta umaskini. Mali ni taji ya fahari ya wenye hekima, lakini ujinga ni shada la wapumbavu. Shahidi wa kweli huokoa maisha, lakini msema uongo ni msaliti. Amchaye Mwenyezi-Mungu ana tumaini imara, na watoto wake watapata kimbilio salama. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni chemchemi ya uhai; humwezesha mtu kuepa mitego ya kifo. Fahari ya mfalme ni wingi wa watu wake, lakini bila watu mtawala huangamia. Mtu asiye mwepesi wa hasira ana busara kubwa, lakini akasirikaye upesi hukuza upumbavu. Amani rohoni humpa mtu afya, lakini tamaa huozesha mifupa. Anayemdhulumu maskini anamtukana Muumba wake, lakini amwoneaye huruma mhitaji anamtukuza Mungu. Mwovu huangamizwa kwa matendo yake maovu, lakini mwadilifu hupata usalama kwa unyofu wake. Hekima imo moyoni mwa mtu mwenye busara; haipatikani kamwe mioyoni mwa wapumbavu. Uadilifu hukuza taifa, lakini dhambi ni balaa kwa taifa lolote. Mfalme humfadhili mtumishi atendaye kwa hekima, lakini hasira yake huwakumba watendao yasiyofaa. Kujibu kwa upole hutuliza hasira, lakini neno kali huchochea hasira. Ulimi wa mwenye hekima hueneza maarifa, lakini watu wapumbavu hububujika upuuzi. Macho ya Mwenyezi-Mungu huona kila kitu, humchunguza mtu mwema na mtu mbaya. Ulimi mpole ni chanzo cha uhai, lakini uovu wake huvunja moyo. Mpumbavu hudharau mafundisho ya baba yake, lakini anayekubali maonyo ana busara. Nyumbani mwa mwadilifu mna wingi wa mali, lakini mapato ya waovu huishia na balaa. Mdomo wa mwenye hekima hueneza maarifa, lakini sivyo ilivyo mioyo ya wapumbavu. Sadaka ya waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, lakini sala ya wanyofu humfurahisha Mungu. Mwenendo wa waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, lakini Mungu huwapenda wale wafuatao mambo adili. Adhabu kali ipo kwa wanaoacha mwenendo mwema; yeyote achukiaye kuonywa atakufa. Ikiwa Mwenyezi-Mungu ajua yaliyo Kuzimu na Abadoni, mawazo ya binadamu yatawezaje kujificha mbele yake? Mwenye madharau hapendi kuonywa, hatafuti kamwe maoni ya wenye busara. Moyo wa furaha hungarisha uso, lakini uchungu huvunja moyo. Mwenye busara hutafuta maarifa, lakini wapumbavu hujilisha upuuzi. Kwa mnyonge kila siku ni mbaya, lakini kwa mwenye moyo mchangamfu ni sikukuu. Afadhali kuwa na kidogo na kumcha Mwenyezi-Mungu, kuliko kuwa na mali nyingi pamoja na taabu. Afadhali mlo wa jioni wa mchicha na upendo, kuliko karamu ya nyama nono pamoja na chuki. Mtu wa hasira mbaya husababisha ugomvi, lakini asiye mwepesi wa hasira hutuliza ugomvi. Njia ya mvivu imesambaa miiba, njia ya mwaminifu ni wazi kama barabara kuu. Mtoto mwenye hekima humfurahisha baba yake, lakini mpumbavu humdharau mama yake. Upumbavu ni furaha kwa mtu asiye na akili, lakini mwenye busara huchagua njia iliyo sawa. Mipango huharibika kwa kukosa shauri, lakini kwa washauri wengi, hufaulu. Kutoa jibu sahihi hufurahisha; neno lifaalo kwa wakati wake ni jema mno! Njia ya mwenye hekima huelekea juu kwenye uhai, ili aepe kuingia chini kuzimu. Mwenyezi-Mungu huyabomoa makao ya wenye kiburi, lakini huilinda mipaka ya makao ya mjane. Mawazo ya mwovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, bali maneno mema humfurahisha. Anayetamani faida ya ulanguzi anaitaabisha jamaa yake, lakini achukiaye hongo ataishi. Moyo wa mwadilifu hufikiri kabla ya kujibu, lakini kinywa cha mwovu hububujika uovu. Mwenyezi-Mungu yuko mbali na watu waovu, lakini yu karibu na watu wema kuwasikiliza. Macho ya huruma hufurahisha moyo, habari njema huuburudisha mwili. Mtu ambaye husikiliza maonyo mema, anayo nafasi yake miongoni mwa wenye hekima. Anayekataa kufundishwa anajidharau mwenyewe, bali anayekubali maonyo hupata busara. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni shule ya hekima; kabla ya kuheshimika ni lazima kuwa mnyenyekevu. Binadamu hupanga mipango yake, lakini kauli ya mwisho ni yake Mwenyezi-Mungu. Matendo ya mtu huonekana kwake kuwa sawa, lakini Mwenyezi-Mungu hupima nia ya mtu. Mwekee Mwenyezi-Mungu kazi yako, nayo mipango yako itafanikiwa. Mwenyezi-Mungu ameumba kila kitu kwa kusudi lake; hata waovu kwa ajili ya siku ya maangamizi. Kila mwenye kiburi ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; hakika mtu wa namna hiyo hataacha kuadhibiwa. Kwa utii na uaminifu mtu huondolewa dhambi, kwa kumcha Mwenyezi-Mungu huepuka uovu. Mwenyezi-Mungu akipendezwa na mwenendo wa mtu, huwageuza hata adui zake kuwa marafiki. Afadhali mali kidogo kwa uadilifu, kuliko mapato mengi kwa udhalimu. Mtu aweza kufanya mipango yake, lakini Mwenyezi-Mungu huongoza hatua zake. Mfalme huamua kwa maongozi ya Mungu; anapotoa hukumu hakosei. Mwenyezi-Mungu hutaka kipimo na mizani halali; mawe yote mfukoni ya kupimia ni kazi yake. Ni chukizo kubwa wafalme kutenda uovu, maana msingi wa mamlaka yao ni haki. Mfalme hupendelea mtu asemaye kwa unyofu; humpenda mtu asemaye ukweli. Hasira ya mfalme ni kama mjumbe wa kifo; mtu mwenye busara ataituliza. Uso wa mfalme ukingaa kuna uhai; wema wake ni kama wingu la masika. Kupata hekima ni bora kuliko dhahabu; kupata akili ni chaguo bora kuliko fedha. Njia ya wanyofu huepukana na uovu; anayechunga njia yake huhifadhi maisha yake. Kiburi hutangulia maangamizi; majivuno hutangulia maanguko. Afadhali kuwa mnyenyekevu na kuwa maskini, kuliko kugawana nyara na wenye kiburi. Anayezingatia mafundisho atafanikiwa; heri mtu yule anayemtumainia Mwenyezi-Mungu. Mwenye hekima moyoni huitwa mwenye akili; neno la kupendeza huwavutia watu. Hekima ni chemchemi ya uhai kwake aliye nayo, bali upumbavu ni adhabu ya wapumbavu. Moyo wa mwenye hekima humwezesha kusema kwa busara; huyafanya maneno yake yawe ya kuvutia. Maneno mazuri ni kama asali; ni matamu rohoni na yenye kuupa mwili afya. Mtu aweza kuona njia yake kuwa sawa, lakini mwishowe humwongoza kwenye kifo. Hamu ya chakula humhimiza mfanyakazi, maana njaa yake humsukuma aendelee. Mtu mwovu hupanga uovu; maneno yake ni kama moto mkali. Mtu mpotovu hueneza ugomvi, mfitini hutenganisha marafiki. Mtu mkatili humshawishi jirani yake; humwongoza katika njia mbaya. Anayekonyeza jicho kwa hila amepanga maovu; anayekaza midomo amekwisha nuia mabaya. Kuwa na mvi za uzee ni taji la utukufu; hupatikana kwa maisha ya uadilifu. Asiye mwepesi wa hasira ni bora kuliko mwenye nguvu; aitawalaye nafsi yake ni bora kuliko autekaye mji. Kura hupigwa kujua yatakayotukia, lakini uamuzi ni wake Mwenyezi-Mungu. Afadhali mkate mkavu kwa amani, kuliko karamu katika nyumba ya ugomvi. Mtumwa mwenye busara atachukua nafasi ya mwana mpumbavu, atapata sehemu ya urithi wa jamaa hiyo. Ubora wa dhahabu ama fedha hupimwa kwa moto, lakini Mwenyezi-Mungu ndiye apimaye mioyo ya watu. Mtenda maovu husikiliza maneno mabaya, mwongo hutegea sikio ulimi mdanganyifu. Anayemdhihaki maskini anamtukana Muumba wake; anayefurahia maafa hatakosa kuadhibiwa. Wazee huwaonea fahari wajukuu zao; watoto huwaonea fahari wazazi wao. Maneno mazuri si kawaida kinywani mwa mpumbavu, sembuse maneno ya uongo kinywani mwa kiongozi! Kwa mhongaji, hongo ni kama hirizi; kila afanyacho hufanikiwa. Anayesamehe makosa hujenga urafiki, lakini anayekumbusha makosa hutenga rafiki. Onyo kwa mwenye busara lina maana, kuliko mapigo mia kwa mpumbavu. Afanyalo mtu mwovu ni kuasi tu; mjumbe mkatili atatumwa dhidi yake. Afadhali kukutana na dubu jike aliyenyanganywa watoto wake, kuliko kukutana na mpumbavu katika upumbavu wake. Mwenye kulipiza mema kwa mabaya, mabaya hayataondoka nyumbani mwake. Kuanzisha ugomvi ni kama kufanya ufa kwenye bwawa; achana na ugomvi kabla haujafurika. Kumsamehe mwenye hatia na kumwadhibu asiye na hatia yote mawili ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu. Ya nini mpumbavu kuwa na fedha mkononi kununulia hekima, wakati yeye mwenyewe hana akili? Rafiki wa kweli ni rafiki siku zote, ndugu huzaliwa asaidie wakati wa taabu. Si jambo la akili kuweka rehani, na kuwa mdhamini wa mtu mwingine. Anayependa ugomvi anapenda dhambi; anayejigamba anajitafutia maangamizi. Mwenye moyo mpotovu hafanikiwi, na msema uongo hupatwa na maafa. Mtoto mpumbavu ni huzuni kwa baba yake, na baba wa mpumbavu hana furaha. Moyo mchangamfu ni dawa, bali moyo wenye huzuni hudhoofisha mwili. Mtu mbaya hupokea hongo kwa siri ili apate kupotosha haki. Mtu mwenye busara lengo lake ni hekima, lakini mpumbavu hupania kila kitu duniani. Mtoto mpumbavu ni huzuni kwa baba yake, na uchungu kwa mama yake mzazi. Si vizuri kumtoza faini mtu asiye na hatia; ni kosa kumchapa viboko muungwana. Asiyesema sana ana maarifa; mtu mtulivu ni mwenye busara. Hata mpumbavu akinyamaza huonekana ana hekima; akifunga mdomo wake huonekana kuwa mwenye akili. Anayetafuta yake tu hujitenga na wenzake; hukasirika akipewa shauri lolote jema. Mpumbavu hapendezwi na busara; kwake cha maana ni maoni yake tu. Ajapo mwovu huja pia dharau; pamoja na aibu huja fedheha. Maneno yaweza kuwa chemchemi ya hekima; yenye kilindi kama bahari, kama kijito kinachobubujika. Si vizuri kumpendelea mtu mwovu, na kumnyima haki mtu mwadilifu. Maneno ya mpumbavu huleta ugomvi; kila anachosema husababisha adhabu. Kinywa cha mpumbavu humwangamiza mwenyewe; mdomo wake ni mtego wa kumnasa yeye mwenyewe. Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo kitamu; ambacho hushuka moja kwa moja mpaka tumboni. Mtu mvivu kazini mwake ni ndugu yake mharibifu. Jina la Mwenyezi-Mungu ni mnara imara; mwadilifu huukimbilia akawa salama. Lakini tajiri hudhani mali ni ngome yake; anafikiri hayo ni ukuta mrefu unaomlinda. Majivuno ya moyoni huleta maangamizi, lakini unyenyekevu huleta heshima. Kujibu kabla ya kusikiliza ni upumbavu na jambo la aibu. Roho ya mtu huweza kustahimili ugonjwa, lakini ukiwa umevunjika moyo, utastahimilije? Mtu mwenye akili hujipatia maarifa, sikio la mwenye busara hutafuta maarifa. Zawadi humfungulia mtu milango; huweza kumfikisha mtu mbele ya mkuu. Ajiteteaye kwanza huonekana msema kweli, mpaka hapo mpinzani wake atakapoanza kumhoji. Kura hukomesha ubishi; huamua kati ya wakuu wanaopingana. Ndugu aliyeudhiwa ni mgumu kuliko mji wa ngome; magomvi hubana kama makufuli ya ngome. Maneno ya mtu yaweza kumshibisha; hutosheka kwa matokeo ya maneno yake. Ulimi una nguvu ya kufanya hai na kuua; wanaopenda kuutumia watakula matunda yake. Anayempata mke amepata bahati njema; hiyo ni fadhili kutoka kwa Mwenyezi-Mungu. Maskini huomba kwa unyenyekevu, bali tajiri hujibu kwa ukali. Marafiki wengi waweza kumwangusha mtu, lakini wapo marafiki waaminifu kuliko ndugu. Afadhali maskini aishiye kwa unyofu, kuliko mtu mpotovu wa maneno na mpumbavu. Haifai mtu kuwa bila akili; mwenda harakaharaka hujikwaa. Mtu akijiangamiza kwa upumbavu wake, huielekeza hasira yake dhidi ya Mwenyezi-Mungu. Mali huvuta marafiki wengi wapya, lakini maskini huachwa bila rafiki. Shahidi mwongo hataacha kuadhibiwa; asemaye uongo hataepa adhabu. Watu wengi hujipendekeza kwa wakuu; kila mtu hutaka kuwa rafiki ya mtu mkarimu. Maskini huchukiwa na ndugu zake; marafiki zake ndio zaidi: Humkimbia! Hata awabembeleze namna gani hatawapata. Ajipatiaye hekima anaipenda nafsi yake; anayezingatia busara atastawi. Shahidi mwongo hatakosa kuadhibiwa; asemaye uongo ataangamia. Haifai kwa mpumbavu kuishi kwa anasa, tena ni vibaya zaidi mtumwa kuwatawala wakuu. Mwenye busara hakasiriki upesi; kusamehe makosa ni fahari kwake. Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba, lakini wema wake ni kama umande juu ya majani. Mtoto mpumbavu ni balaa kwa baba yake; na ugomvi wa mke ni kama matone ya mvua yasiyoisha. Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa wazee wake, lakini mke mwenye busara hutoka kwa Mwenyezi-Mungu. Uzembe ni kama usingizi mzito; mtu mvivu atateseka kwa njaa. Anayeshika amri anasalimisha maisha yake; anayepuuza agizo atakufa. Anayemsaidia maskini anamkopesha Mwenyezi-Mungu; Mwenyezi-Mungu atamlipa kwa tendo lake jema. Mrudi mwanao kungali bado na tumaini, lakini usimwadhibu kiasi cha kumwangamiza. Mtu wa hasira kali lazima apate adhabu; ukimwachia mara moja itakubidi kumwachia tena. Sikiliza shauri na kupokea mafundisho, upate hekima ya kukufaa siku zijazo. Kichwani mwa mtu mna mipango mingi, lakini anachokusudia Mwenyezi-Mungu ndicho kitakachofanyika. Kinachotakiwa kwa mtu ni uaminifu; afadhali mtu maskini kuliko mtu mwongo. Kumcha Mwenyezi-Mungu kunaleta uhai; amchaye hujaliwa pumziko la kutosheleza, wala hatapatwa na baa lolote. Mvivu ni kama mtu atiaye mkono katika sahani ya chakula, lakini hana nguvu ya kuuinua hadi mdomoni. Mwadhibu mwenye mzaha naye mjinga atapata akili; mwonye mwenye busara naye atapata maarifa. Anayemdhulumu baba yake na kumfukuza mama yake, ni mtoto asiyefaa na mpotovu. Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho, utapotea mara mbali na maneno ya hekima. Shahidi asiyefaa kitu huidhihaki haki; na kinywa cha mwovu hubugia uovu. Adhabu iko tayari kwa wenye mzaha, mijeledi imetayarishwa kuchapa migongo ya wapumbavu. Divai huleta dhihaka na kileo huleta ugomvi; yeyote anayevutiwa navyo hana hekima. Ghadhabu kali ya mfalme ni kama simba angurumaye; anayemkasirisha anayahatarisha maisha yake. Ni jambo la heshima kuepa ugomvi; wapumbavu ndio wanaogombana. Mvivu halimi wakati wa kulima; wakati wa mavuno atatafuta asipate chochote. Fikira za mtu zimefichika kama kilindi cha maji; lakini mtu mwenye busara ajua kuzichota humo. Watu wengi hujivunia kuwa wema, lakini mwaminifu wa kweli apatikana wapi? Mtu mwadilifu akiishi kwa unyofu; watoto wake atakaowaacha watabarikiwa. Mfalme mwema aketipo kutoa hukumu, huupepeta uovu wote kwa macho yake. Nani athubutuye kusema: “Nimeutakasa moyo wangu; mimi nimetakasika dhambi yangu?” Mizani ya udanganyifu na vipimo vya udanganyifu, vyote ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu. Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni njema na aminifu. Sikio lisikialo na jicho lionalo, yote mawili kayafanya Mwenyezi-Mungu. Usipende kulala tu usije ukawa maskini; uwe macho nawe utakuwa na chakula kingi. “Hakifai, hakifai”, mnunuzi hulalamika, lakini akiondoka hujisifu amepunguziwa bei. Kuna dhahabu na wingi wa mawe ya thamani kubwa; lakini cha thamani kubwa zaidi ni maneno ya busara! Mtu akiahidi mbele yako kumdhamini mgeni, chukua nguo yake; mfanye awajibike kwa kuwadhamini wageni. Chakula kipatikanacho kwa udanganyifu ni kitamu, lakini baadaye huwa kama mchanga kinywani. Mipango mizuri hufanyika kwa kushauriana; ukitaka kuanza vita lazima kutafakari kwanza. Mpiga domo hafichi siri, kwa hiyo mwepe mtu wa kuropoka. Anayemlaani baba yake au mama yake, mwanga wa uhai wake utazimwa kama taa gizani. Mali iliyopatikana kwa haraka mwanzoni, haitakuwa ya heri mwishoni. Usiseme, “Nitalipiza ubaya niliotendewa.” Mtegemee Mwenyezi-Mungu naye atakusaidia. Mizani ya udanganyifu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, na vipimo visivyo halali ni kitu kibaya. Hatua za mtu huongozwa na Mwenyezi-Mungu; awezaje binadamu kujua njia ya kwenda? Ni hatari kusema kwa mzaha “Usiahidi kumpa Mungu kitu bila kufikiri, la sivyo utaanza kusikitika baada ya nadhiri yako.” Mfalme mwenye busara huwapepeta waovu; huwaadhibu bila huruma. Dhamiri ya mtu ni taa ya Mwenyezi-Mungu; huchunguza nafsi yake mtu mpaka ndani kabisa. Wema na uaminifu humkinga mfalme; utawala wake huimarishwa kwa uadilifu. Fahari ya vijana ni nguvu zao, uzuri wa vikongwe ni mvi za uzee. Mapigo yanayoumiza ni dawa ya kuondoa uovu; viboko husafisha nafsi mpaka ndani kabisa. Moyo wa mfalme ni kama maji yanayotiririka; Mwenyezi-Mungu, huuongoza popote apendapo. Matendo yote ya mtu ni sawa machoni pake, lakini Mwenyezi-Mungu hupima mioyo. Kutenda mambo mema na ya haki, humpendeza Mwenyezi-Mungu kuliko tambiko. Macho ya kiburi na moyo wa majivuno huonesha wazi dhambi ya waovu. Mipango ya mtu wa bidii huleta mali kwa wingi, lakini kila aliye na pupa huishia patupu. Mali ipatikanayo kwa udanganyifu, ni mvuke upitao na mtego wa kifo. Ukatili wa wakatili utawafutilia mbali, maana wanakataa kutenda yaliyo ya haki. Njia ya mtu mwenye hatia imepotoka, lakini mwenendo wa mnyofu umenyooka. Afadhali kuishi pembeni juu ya paa, kuliko kuishi nyumbani na mwanamke mgomvi. Anachopania kutenda mtu mbaya ni uovu; hata kwa jirani yake hana huruma. Ukimwadhibu mwenye dhihaka, mjinga hupata hekima; ukimfundisha mwenye hekima, unampatia maarifa. Mungu Mwadilifu anajua wanayotenda waovu nyumbani kwao; naye atawaangusha na kuwaangamiza. Anayekataa kusikiliza kilio cha maskini, naye pia hatasikilizwa atakapolilia msaada. Hasira hutulizwa kwa zawadi ya siri; tunu apewayo mtu imefichwa hupooza ghadhabu. Haki ikitekelezwa watu wema hufurahi, lakini watu waovu hufadhaishwa. Anayetangatanga mbali na njia ya busara, atajikuta ametua miongoni mwa wafu. Anayependa anasa atakuwa maskini; anayefikiria tu kula na kunywa hatatajirika. Mwovu atapata pigo ambalo halitampata mtu mwema, mkosefu ataadhibiwa badala ya mnyofu. Afadhali kuishi jangwani, kuliko kukaa na mwanamke mgomvi na msumbufu. Nyumbani kwa mwenye busara mna hazina za thamani, lakini mpumbavu huponda mali yake yote. Anayepania uadilifu na huruma, ataishi maisha marefu na kuheshimiwa. Mwenye hekima aweza kuteka mji wa wenye nguvu, na kuziporomosha ngome wanazozitegemea. Achungaye mdomo wake na ulimi wake, hujiepusha na matatizo. Mwenye majivuno na kiburi jina lake ni “Madharau;” matendo yake yamejaa majivuno ya ufidhuli wake. Mvivu hufa kwa kutotimizwa tamaa zake, maana mikono yake milegevu haitaki kufanya kazi. Mchana kutwa mwovu hutamani kupata kitu, lakini mwadilifu hutoa, tena kwa ukarimu. Tambiko ya mwovu ni kitu cha kuchukiza, huchukiza zaidi akiitoa kwa nia mbaya. Shahidi mwongo ataangamia, lakini msikivu hawezi kunyamazishwa. Mtu mwovu hujionesha kuwa jasiri, lakini mwadilifu huhakikisha ametenda sawa. Hakuna hekima, maarifa, wala mawaidha yoyote ya mtu, yawezayo kumshinda Mwenyezi-Mungu. Farasi hutayarishwa kwa vita, lakini ushindi wamtegemea Mwenyezi-Mungu. Afadhali kuwa na sifa nzuri kuliko mali nyingi; wema ni bora kuliko fedha au dhahabu. Matajiri na maskini wana hali hii moja: Mwenyezi-Mungu ni Muumba wao wote. Mtu mwangalifu huona hatari akajificha, lakini wajinga hujitokeza mbele wakaumia. Ukinyenyekea na kumcha Mwenyezi-Mungu, utapata tuzo: Fanaka, heshima na uhai. Njia ya waovu imejaa miiba na mitego; anayetaka kuhifadhi maisha yake ataiepa. Mfunze mtoto namna ya kuishi vizuri, naye hatasahau njia hiyo hata uzeeni. Tajiri humtawala maskini; mkopaji ni mtumwa wa mkopeshaji. Apandaye dhuluma atavuna janga; uwezo wake wa kutenda mabaya utavunjwa. Mtu mkarimu atabarikiwa, maana chakula chake humgawia maskini. Mfukuze mwenye dharau na fujo itatoweka, ugomvi na matusi vitakoma. Mwenye nia safi na maneno mazuri, atakuwa rafiki wa mfalme. Mwenyezi-Mungu hulinda elimu ya kweli, lakini huyavuruga maneno ya waovu. Mvivu husema, “Siwezi kutoka nje; kuna simba huko, ataniua!” Kinywa cha mwasherati ni shimo refu; anayechukiwa na Mwenyezi-Mungu atatumbukia humo. Mtoto hupenda mambo ya kijinga moyoni, lakini fimbo ya nidhamu humwondolea hayo. Anayemdhulumu maskini atamfanya afaidike mwishowe, anayewapa matajiri zawadi ataishia kuwa maskini. Tega sikio usikie maneno ya wenye hekima, elekeza moyo wako uzingatie maarifa yangu. Wewe utafurahi endapo utayaweka moyoni, na kuyakariri kila wakati. Ninayependa kumfundisha leo ni wewe, ili tegemeo lako liwe kwa Mwenyezi-Mungu. Nimekuandikia misemo thelathini, misemo ya maonyo na maarifa, ili kukufundisha yaliyo sawa na kweli; na mtu akikuuliza uweze kumpa jibu sahihi. Usimdhulumu maskini kwa kuwa ni maskini, wala usimnyime fukara haki yake mahakamani. Maana Mwenyezi-Mungu atawatetea; atawapokonya maisha yao wale watakaowadhulumu. Usifanye urafiki na mtu wa hasira, wala usiandamane na mwenye ghadhabu, usije ukajifunza mwenendo wake, ukajinasa kabisa katika mtego. Usiwe mmoja wao wenye kuweka ahadi, watu ambao hujiweka wadhamini wa madeni. Ikiwa huna chochote cha kulipa, hata kitanda unacholalia kitachukuliwa! Usiondoe alama ya mipaka ya zamani ambayo iliwekwa na wazee wako. Je, yuko mtu mwenye maarifa kazini mwake? Huyo atawatumikia wafalme; hatawapa huduma yake watu wasiofaa. Ukiketi kula pamoja na mtawala, usisahau hata kidogo uko pamoja na nani. Zuia sana hamu yako, ikiwa wewe wapenda sana kula. Usitamani vyakula vyake vizuri, maana vyaweza kukudanganya. Ikiwa unayo hekima ya kutosha, usijitaabishe kutafuta utajiri. Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka, huwa kama umepata mabawa ghafla, ukaruka na kutowekea angani kama tai. Usile chakula cha mtu bahili, wala usitamani mapochopocho yake, maana moyoni mwake anahesabu unachokula. Atakuambia, “Kula, kunywa!” Lakini moyoni mwake hayuko pamoja nawe. Utatapika vipande ulivyokula; shukrani zako zote zitakuwa za bure. Usiseme maneno yako mbele ya mpumbavu, maana atapuuza hekima ya maneno yako. Usiondoe alama ya mpaka wa zamani, wala usiingilie mashamba ya yatima, maana Mungu, Mkombozi, ni mwenye nguvu, naye ataitetea haki yao dhidi yako. Tumia akili zako kufuata mafundisho; tumia masikio yako kusikiliza maarifa. Usiache kumrudi mtoto; ukimchapa kiboko hatakufa. Ukimtandika kiboko, utayaokoa maisha yake na kuzimu. Mwanangu, moyo wako ukiwa wenye busara, moyo wangu pia utakuwa wenye furaha. Moyo wangu utashangilia, mdomo wako utakaposema maneno yaliyo sawa. Moyo wako usiwaonee wivu wenye dhambi, ila endelea kumcha Mwenyezi-Mungu siku zote. Hakika kuna kesho ya milele, na tumaini lako halitakuwa bure. Sikia mwanangu, uwe na hekima; fikiria sana jinsi unavyoishi. Usiwe mmoja wa walevi wa divai, wala walafi wenye kupenda nyama, maana walevi na walafi wataishia kuwa maskini, anayetumia siku yake kusinzia atavaa matambara. Msikilize baba yako aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako akizeeka. Nunua ukweli, wala usiuuze; nunua hekima, mafunzo na busara. Baba wa mtoto mwadilifu atajaa furaha; anayemzaa mtoto mwenye hekima atamfurahia. Wafurahishe baba na mama yako; mama aliyekuzaa na afurahi. Mwanangu, nisikilize kwa makini, shikilia mwenendo wa maisha yangu. Malaya ni shimo refu la kutega watu; mwanamke mgeni ni kama kisima chembamba. Yeye hunyemelea kama mnyanganyi, husababisha wanaume wengi kukosa uaminifu. Ni nani wapigao yowe? Ni nani wenye huzuni? Ni nani wenye ugomvi? Ni nani walalamikao? Ni nani wenye majeraha bila sababu? Ni nani wenye macho mekundu? Ni wale ambao hawabanduki penye divai, wale wakaao chonjo kuonja divai iliyokolezwa. Usiitamani divai hata kwa wekundu wake, hata kama inametameta katika bilauri, na kushuka taratibu unapoinywa. Mwishowe huuma kama nyoka; huchoma kama nyoka mwenye sumu. Macho yako yataona mauzauza, moyo wako utatoa mambo yaliyopotoka. Utakuwa kama mtu alalaye katikati ya bahari, kama mtu alalaye juu ya mlingoti wa meli. Utasema, “Walinichapa, lakini sikuumia; walinipiga, lakini sina habari. Nitaamka lini? Ngoja nitafute kinywaji kingine!” Usiwaonee wivu watu waovu, wala usitamani kuwa pamoja nao, maana fikira zao zote ni juu ya ukatili, hamna jema lolote litokalo midomoni mwao. Nyumba hujengwa kwa hekima, na kuimarishwa kwa busara. Kwa maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vya thamani na vya kupendeza. Kuwa na hekima ni bora kuliko kuwa na nguvu, naam, maarifa ni bora kuliko nguvu. Maana kwa mwongozo mzuri waweza kupigana vita, na kwa washauri wengi ushindi hupatikana. Kwa mpumbavu hekima ni ngumu kuielewa; penye mkutano wa mashauri hafungui mdomo. Afikiriaye kutenda maovu daima ataitwa mtu mwenye fitina. Mpango anaofikiria mpumbavu ni dhambi; mwenye dharau huchukiwa na kila mtu. Ukifa moyo wakati wa shida, basi wewe ni dhaifu kweli. Mwokoe mtu anayechukuliwa kuuawa bure; usisite kumwokoa anayeuawa bila hatia. Usiseme baadaye: “Hatukujua!” Maana Mungu apimaye mioyo ya watu huona; yeye atakulipa kulingana na matendo yako! Mwanangu, ule asali maana ni nzuri; sega la asali ni tamu mdomoni. Ndivyo ilivyo hekima nafsini mwako; ukiipata utakuwa na matazamio mema, wala tumaini lako halitakuwa la bure. Usivizie kama mwovu kushambulia makao ya mtu mwema, wala usijaribu kuiharibu nyumba yake, maana mtu mwema huanguka mara nyingi lakini huinuka, lakini mtu mwovu huangamizwa na janga. Usishangilie kuanguka kwa adui yako; usifurahie moyoni mwako kujikwaa kwake, maana Mwenyezi-Mungu aonaye hayo hatapendezwa; huenda akaacha kumwadhibu. Usihangaike kwa sababu ya watenda mabaya, wala usiwaonee wivu watu waovu, maana mwovu hatakuwa na mema baadaye; taa ya uhai wake itazimwa. Mwanangu, umche Mwenyezi-Mungu na kumheshimu mfalme, wala usishirikiane na wale wasio na msimamo, maana maangamizi yao huwapata ghafla. Hakuna ajuaye maafa watakayozusha. Ifuatayo pia ni misemo ya wenye hekima: Kupendelea watu katika hukumu si vizuri. Anayemwachilia mtu mwenye hatia, hulaaniwa na watu na kuchukiwa na mataifa. Lakini wanaowaadhibu waovu watapata furaha, na baraka njema zitawajia. Jibu lililo la haki, ni kama busu la rafiki. Kwanza fanya kazi zako nje, tayarisha kila kitu shambani, kisha jenga nyumba yako. Usishuhudie bure dhidi ya jirani yako, wala usiseme uongo juu yake. Usiseme, “Nitamtenda kama alivyonitenda! Ni lazima nilipize kisasi!” Nilipitia karibu na shamba la mvivu; shamba la mzabibu la mtu mpumbavu. Nilishangaa kuona limemea miiba, magugu yamefunika eneo lake lote, na ukuta wake wa mawe umebomoka. Nilitazama, nikawaza, mwishowe nikapata funzo: Lala tu kidogo; sinzia tu kidogo! Kunja mikono yako tu upumzike! Lakini kumbuka kwamba uwapo usingizini, umaskini utakuvamia kama mnyanganyi, ufukara kama mtu mwenye silaha. Hizi nazo ni methali nyingine za mfalme Solomoni walizonakili watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda. Mungu hutukuzwa kwa kuficha mambo, lakini mfalme hutukuzwa kwa yale anayoeleza. Kama zilivyo mbali mbingu na kirefu kina cha ardhi ndivyo zisivyochunguzika akili za mfalme. Toa takataka katika fedha, na mhunzi atakutengenezea chombo kizuri. Waondoe waovu mbele ya mfalme, na utawala wake utaimarika katika haki. Usijipendekeze kwa mfalme, wala usijifanye mtu mkubwa, maana ni heri kuambiwa, “Njoo huku mbele”, kuliko kuporomoshwa mbele ya mkuu. Mambo uliyoyaona kwa macho yako, usiharakishe kuyapeleka mahakamani; maana utafanya nini hapo baadaye, shahidi mwingine akibatilisha hayo usemayo? Suluhisha ugomvi na mwenzako peke yake, na kila mmoja wenu asitoe siri ya mwenzake; watu wasije wakajua kuna siri, ukajiharibia jina lako daima. Neno lisemwalo wakati unaofaa, ni kama nakshi za dhahabu juu ya madini ya fedha. Onyo la mwenye hekima kwa mtu msikivu, ni bora kuliko pete au vito vya dhahabu safi. Mjumbe mwaminifu humfurahisha yule aliyemtuma, kama maji baridi wakati wa joto la mavuno. Kama vile mawingu na upepo bila mvua, ndivyo alivyo mtu anayejigamba kutoa zawadi asiitoe. Kwa uvumilivu mtawala huweza kushawishika; ulimi laini huvunja mifupa. Upatapo asali kula kiasi cha kukutosha, usije ukaikinai na kuitapika. Usimtembelee jirani yako mara kwa mara, usije ukamchosha naye akakuchukia. Mtu atoaye ushahidi wa uongo dhidi ya mwenziwe, ni hatari kama rungu, upanga au mshale mkali. Kumtegemea mtu asiyeaminika wakati wa taabu, ni kama jino bovu au mguu ulioteguka. Kumwimbia mtu mwenye huzuni, ni kama kuvua nguo wakati wa baridi, au kutia siki katika kidonda. Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe maji ya kunywa. Hivyo utafanya apate aibu kali, kama makaa ya moto kichwani pake, naye Mwenyezi-Mungu atakutuza. Upepo wa kusi huleta mvua, hali kadhalika masengenyo huleta chuki. Afadhali kuishi pembeni juu ya paa, kuliko kuishi nyumbani pamoja na mwanamke mgomvi. Kama vile maji baridi kwa mwenye kiu, ndivyo habari njema kutoka mbali. Mwadilifu akubaliye kufuata mambo ya mwovu, ni chemchemi iliyochafuliwa au kisima kilichotibuliwa. Si vizuri kula asali nyingi mno; kadhalika haifai kujipendekeza mno. Mtu asiyeweza kuzuia hasira yake, ni kama mji usio na ulinzi unaposhambuliwa. Heshima apewayo mpumbavu haimfai; ni kama theluji ya kiangazi, au mvua ya wakati wa mavuno. Kama shomoro au mbayuwayu wasiotua, kadhalika laana asiyostahili mtu haimtui. Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda, na fimbo kwa mgongo wa mpumbavu. Usimjibu mpumbavu kipumbavu, usije ukafanana naye. Mjibu mpumbavu kama ustahilivyo upumbavu wake, asije akajiona kuwa mwenye hekima zaidi. Kumtuma mpumbavu ujumbe, ni kama kujikata miguu au kujitafutia shida. Methali mdomoni mwa mpumbavu, ni kama miguu ya kiwete inayoninginia. Kumpa mpumbavu heshima, ni kama kufunga jiwe kwenye kombeo. Mpumbavu anayejaribu kutumia methali, ni kama mlevi anayejaribu kungoa mwiba mkononi. Mtu amwajiriye mpumbavu au mlevi, ni kama mpiga upinde anayejeruhi kila mtu. Mpumbavu anayerudiarudia upumbavu wake, ni kama mbwa anayekula matapishi yake. Wamwona mtu ajionaye kuwa mwenye hekima? Nakuambia mpumbavu ni nafuu kuliko huyo. Mvivu husema: “Huko nje kuna simba; siwezi kwenda huko.” Kama vile mlango uzungukiapo bawaba zake, ndivyo mvivu juu ya kitanda chake. Mvivu huutia mkono wake katika sahani ya chakula, lakini hawezi kuuinua hadi mdomoni. Mvivu hujiona kuwa mwenye hekima kuliko watu saba wawezao kujibu kwa busara. Ajiingizaye katika ugomvi usiomhusu, ni kama mtu amshikaye masikio mbwa anayepita. Kama mwendawazimu achezeavyo mienge, au mishale ya kifo, ndivyo alivyo mtu ampotoshaye jirani, kisha aseme, “Nilikuwa natania tu!” Bila kuni, moto huzimika; bila mchochezi, ugomvi humalizika. Kama vile makaa au kuni huchochea moto, ndivyo mgomvi achocheavyo ugomvi. Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo; hushuka mpaka ndani kabisa tumboni. Kama rangi angavu iliyopakwa kigae, ndivyo yalivyo maneno matamu yenye nia mbaya. Mwenye chuki huficha chuki yake kwa maneno mazuri, lakini huwa ana hila moyoni mwake. Akiongea vizuri usimwamini, moyoni mwake mna chuki chungu nzima. Huenda akaficha chuki yake, lakini nia zake mbaya zitajulikana kwa wote. Amchimbiaye mwenzake shimo, hutumbukia mwenyewe; abingirishaye jiwe litamrudia mwenyewe. Asemaye uongo huwachukia hao anaowaumiza, naye abembelezaye huleta maangamizi. Usijisifie ya kesho, hujui nini kitatokea leo mpaka kesho. Acha watu wengine wakusifu, kuliko mdomo wako wewe mwenyewe. Jiwe ni zito na mchanga kadhalika, lakini usumbufu wa mpumbavu ni mzito zaidi. Ghadhabu ni katili na hasira huangamiza; lakini ni nani awezaye kuukabili wivu? Afadhali mtu anayekuonya waziwazi, kuliko yule afichaye upendo. Makaripio ya rafiki yaonesha uaminifu, lakini busu la adui ni udanganyifu. Aliyeshiba hata asali huikataa, lakini kwa mwenye njaa kila kichungu ni kitamu. Mtu aliyepotea mbali na kwake, ni kama ndege aliyepotea mbali na kiota chake. Mafuta na manukato huufurahisha moyo, lakini taabu hurarua roho. Usisahau rafiki zako wala wa baba yako. Ukipatwa na janga usikimbilie kwa nduguyo; afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali. Uwe na hekima mwanangu upate kunifurahisha moyo, nami sitakosa la kumjibu yeyote anayenilaumu. Mwenye busara huona hatari akajificha, lakini mjinga hujitokeza mbele akaumia. Mtu akiahidi mbele yako kumdhamini mgeni, chukua nguo yake; mfanye awajibike kwa kuwadhamini wageni. Amwamkiaye jirani kwa kelele alfajiri, itaeleweka kwamba amemtakia laana. Mke mgomvi daima, ni sawa na tonatona ya maji siku ya mvua. Kumzuia ni sawa na kuzuia upepo, au kukamata mafuta kwa mkono. Chuma hunoa chuma, kadhalika mtu hufundishwa na wenzake. Anayeutunza mtini hula tini, anayemhudumia bwana wake ataheshimiwa. Kama uso ujionavyo wenyewe majini, ndivyo ujijuavyo mwenyewe moyoni. Kuzimu na Uharibifu kamwe havishibi, kadhalika na macho ya watu hayashibi. Ubora wa fedha au dhahabu hupimwa kwa moto, na mtu hupimwa kutokana na sifa zake. Mtwange mpumbavu katika kinu pamoja na nafaka, lakini hutafaulu kumtenganisha na upumbavu wake. Angalia vizuri hali ya mifugo yako; tunza vizuri wanyama wako. Maana utajiri haudumu milele, wala taji haidumu vizazi vyote. Baada ya kukata nyasi na kuzihifadhi, kata majani toka milimani, huku nyasi zinachipua upya. Kondoo watakupatia sufu kwa mavazi, mbuzi nao utauza na kujinunulia mashamba; watakupa maziwa ya kukutosha wewe na jamaa yako, na kwa ajili ya watumishi wako wa kike. Waovu hukimbia japo hawafukuzwi na mtu, lakini waadilifu ni hodari kama simba. Taifa la fujo huzusha viongozi wengi, lakini kwa kiongozi mmoja mwenye akili na maarifa huwa na utengemano Mtu mhitaji anayewadhulumu maskini, amefanana na mvua kubwa inayoharibu mimea. Watu wanaovunja sheria huwasifu waovu, lakini wanaoishika sheria hupingana nao. Waovu hawajui maana ya haki, lakini wamchao Mwenyezi-Mungu wanaielewa kabisa. Afadhali maskini aishiye kwa unyofu, kuliko tajiri aishiye kwa upotovu. Mtoto ashikaye sheria ni mwenye hekima, lakini rafiki wa walafi humwaibisha baba yake. Aongezaye mali yake kwa riba na kutoza faida anamkusanyia mwingine mwenye kuwahurumia maskini. Anayekataa kuisikia sheria, huyo hata sala yake ni chukizo kwa Mungu. Anayemshawishi mtu mwema kutenda mabaya, ataanguka katika shimo lake mwenyewe. Wasio na hatia wamewekewa mema yao. Tajiri hujiona mwenyewe kuwa mwenye hekima, lakini maskini mwenye busara atamfichua. Watu wema wakipata madaraka maisha hufana, lakini waovu wakitawala watu hujificha. Afichaye makosa yake hatafanikiwa; lakini anayeungama na kuyaacha atapata rehema. Heri mtu amchaye Mwenyezi-Mungu daima; lakini mkaidi wa moyo ataangukia maafa. Mtawala mwovu anayewatawala maskini, ni kama simba angurumaye au dubu anayeshambulia. Mtawala asiye na akili ni mdhalimu mkatili; lakini achukiaye mali ya udanganyifu atatawala muda mrefu. Mtu anayelemewa na hatia ya kuua mtu, atakuwa mkimbizi mpaka kaburini; mtu yeyote na asijaribu kumzuia. Aishiye kwa unyofu atasalimishwa, lakini mdanganyifu ataanguka kabisa. Anayelima shamba lake atapata chakula kingi, bali anayefuata yasiyofaa atapata umaskini tele. Mtu mwaminifu atapata baraka tele, lakini mwenye pupa ya kuwa tajiri hataepa adhabu. Si vizuri kumbagua mtu; watu hufanya mabaya hata kwa kipande cha mkate. Mtu bahili hukimbilia mali, wala hajui kwamba ufukara utamjia. Amwonyaye mwenzake hatimaye hupata mema zaidi, kuliko yule anayembembeleza kwa maneno matamu. Anayeiba mali ya baba yake au mama yake, akasema si kosa, hana tofauti yoyote na wezi wengine. Mchoyo huchochea ugomvi, lakini anayemtegemea Mwenyezi-Mungu atafanikiwa. Anayetegemea akili yake mwenyewe ni mpumbavu; lakini anayeishi kwa hekima atakuwa salama. Aliye mkarimu kwa maskini hatatindikiwa kitu, lakini anayekataa kuwaangalia atalaaniwa kwa wingi. Waovu wakitawala watu hujificha, lakini wakiangamia, waadilifu huongezeka. Anayeonywa mara nyingi akawa mkaidi, ataangamia ghafla asipone tena. Waadilifu wakitawala watu hufurahi, lakini waovu wakitawala watu hulalamika. Apendaye hekima humfurahisha baba yake; lakini aandamanaye na malaya hufuja mali yake. Mfalme akitumia haki huipatia nchi uthabiti, lakini akipenda hongo taifa huangamia. Mwenye kumbembeleza jirani yake, anatega mtego wa kujinasa mwenyewe. Mtu mbaya hunaswa kwa kosa lake, lakini mtu mwadilifu huimba na kufurahi. Mwadilifu anajua haki za maskini, lakini mtu mwovu hajui mambo hayo. Wenye dharau huutia vurugu mji mzima, lakini wenye hekima hutuliza ghadhabu. Mwenye hekima akibishana na mpumbavu, mpumbavu huwaka hasira na kucheka bila kutulia. Wapendao kumwaga damu humchukia mtu asiye na hatia, lakini watu wema huyalinda maisha yake. Mpumbavu huonesha hasira yake wazi, lakini mwenye hekima huizuia na kuituliza. Mtawala akisikiliza mambo ya uongo, maofisa wake wote watakuwa waovu. Maskini na mkandamizaji wanafanana kwa kitu kimoja: Wote wawili wamepewa macho na Mwenyezi-Mungu. Mfalme anayewaamua maskini kwa haki, atauona utawala wake umeimarika milele. Adhabu na maonyo huleta hekima, lakini mtoto aliyeachwa afanye apendavyo humwaibisha mama yake. Waovu wakitawala maovu huongezeka, lakini waadilifu watashuhudia kuanguka kwao. Mpe nidhamu mwanao naye hatakupa wasiwasi; yeye ataufurahisha moyo wako. Pasipo maono ya kinabii watu hukosa nidhamu; heri mtu yule anayeshika sheria. Mtumwa haonyeki kwa maneno matupu, maana ingawa anayaelewa yeye hatayatii. Wamwona mtu apayukaye bila kufikiri? Mtu mpumbavu ni afadhali kuliko yeye. Ambembelezaye mtumwa wake tangu utoto, mwishowe mtumwa huyo atamrithi. Mwenye ghadhabu huchochea ugomvi, mtu wa hasira husababisha makosa mengi. Kiburi cha mtu humporomosha mwenyewe, lakini mnyenyekevu wa roho atapata heshima. Anayeshirikiana na mwizi anajidhuru mwenyewe; husikia laana ya aliyeonewa bila kusema neno. Kuwaogopa watu ni kujitega mwenyewe, lakini anayemtumaini Mwenyezi-Mungu yu salama. Wengi hupenda kujipendekeza kwa mtawala, hali mtu hupata haki yake kwa Mwenyezi-Mungu. Mdhalimu ni chukizo kwa mnyofu, naye mnyofu ni chukizo kwa mwovu. Maneno ya Aguri, mwana wa Yake. Mawaidha ambayo mtu huyu alimwambia Ithieli, naam, Ithieli na Ukali. Mimi ni mpumbavu mno, wala si mtu; nayo akili ya binadamu sina. Sijajifunza hekima, wala sijui kitu juu ya Mungu Mtakatifu. Ni nani aliyepanda juu mbinguni akashuka chini? Ni nani aliyekamata upepo mkononi? Ni nani aliyefunga maji katika kitambaa? Ni nani aliyeiweka mipaka yote ya dunia? Jina lake ni nani? Na ni nani jina la mwanawe? Niambie kama wajua! Maneno yote ya Mungu ni ya kuaminika; yeye ni ngao yao wote wanaomkimbilia. Usiongeze neno katika maneno yake, asije akakukemea, nawe ukaonekana mwongo. Mambo haya mawili nakuomba ee Mungu, wala usinikatalie kabla sijafa: Uniondolee uongo na udanganyifu; usinipe umaskini wala utajiri; unipatie chakula ninachohitaji, nisije nikashiba nikakukana; nikasema, “Mwenyezi-Mungu ni nani?” Au nisije nikawa maskini nikaiba, na kulikufuru jina lako ee Mungu wangu. Usimchongee mtumwa kwa bwana wake, asije akakulaani, ukaonekana una hatia. Kuna watu ambao huwalaani baba zao, wala hawana shukrani kwa mama zao. Kuna watu ambao hujiona kuwa wema, kumbe bado hawajatakaswa uchafu wao. Kuna na wengine — kiburi ajabu! Hudharau kila kitu wanachokiona. Kuna watu ambao meno yao ni kama upanga, na magego yao ni kama visu. Wako tayari kuwatafuna maskini wa nchi, na wanyonge walio miongoni mwa watu! Mruba anao binti wawili wasemao, “Nipe, nipe!” Kuna vitu vitatu ambavyo kamwe havishibi, naam, vitu vinne visivyosema, “Imetosha!” Kuzimu, tumbo la mwanamke lisilozaa, ardhi isiyoshiba maji, na moto usiosema, “Imetosha!” Kama mtu akimdhihaki baba yake, na kudharau utii kwa mama yake, kunguru wa bondeni watamdonoa macho, na kuliwa na tai. Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu, naam, mambo manne nisiyoyaelewa: Njia ya tai angani, njia ya nyoka mwambani, njia ya meli baharini, na kinachomvuta mwanamume kwa mwanamke. Mwenendo wa mwanamke mwasherati ni hivi: Yeye hula, akajipangusa mdomo, na kusema, “Sijafanya kosa lolote!” Kuna mambo matatu ambayo huitetemesha dunia, naam, mambo manne ambayo haiwezi kuyastahimili: Mtumwa anayekuwa mfalme; mpumbavu anayeshiba chakula; mwanamke asiyependwa anayeolewa; na mjakazi achukuapo nafasi ya bibi yake. Kuna viumbe vinne vidogo sana duniani, lakini vina akili sana: Sisimizi: Wadudu wasio na nguvu, lakini hujihifadhia chakula wakati wa kiangazi; pelele: Wanyama wasio na uwezo, lakini hujitengenezea makao miambani; nzige: Hawana mfalme, lakini wote huenda pamoja kwa vikosi; mjusi: Waweza kumshika mkononi, lakini huingia katika ikulu. Kuna viumbe vitatu vyenye mwendo wa kupendeza, naam, kuna viumbe vinne vyenye mwendo mzuri; simba: Mnyama mwenye nguvu kuliko wote, wala hamwogopi mnyama mwingine yeyote; jogoo aendaye kwa maringo; tena beberu; na mfalme mbele ya watu wake. Kama umekuwa mpumbavu hata ukajisifu, au kama umekuwa unapanga maovu, chunga mdomo wako. Maana ukisukasuka maziwa utapata siagi, ukimpiga mtu pua atatoka damu; kadhalika kuchochea hasira huleta ugomvi. Maneno ya mfalme Lemueli. Mawaidha aliyofundishwa na mama yake: Nikuambie nini mwanangu? Nikuambie nini mwanangu niliyekuzaa? Nikuambie nini wewe niliyekuomba kwa Mungu? Usimalize nguvu zako kwa wanawake, usiwape mali yako hao wanaoangamiza wafalme. Haifai ee Lemueli, haifai wafalme kunywa divai, wala wakuu kutamani vileo. Wakinywa watasahau maagizo ya sheria, na kuwanyima haki wenye taabu. Mpe kileo mtu anayekufa, wape divai wale wenye huzuni tele; wanywe na kusahau umaskini wao, wasikumbuke tena taabu yao. Lakini wewe, lazima useme kwa ajili ya wote walio bubu; na kutetea haki za wote wasiojiweza. Sema kwa ajili yao na kuamua kwa haki, linda haki za maskini na fukara. Mke mwema kweli, apatikana wapi? Huyo ana thamani kuliko johari! Mumewe humwamini kwa moyo, kwake atapata faida daima. Kamwe hamtendei mumewe mabaya, bali humtendea mema maisha yake yote. Hutafuta sufu na kitani, na kufanya kazi kwa mikono yake kwa bidii. Yeye ni kama meli za biashara: Huleta chakula chake kutoka mbali. Huamka kabla ya mapambazuko, akaitayarishia jamaa yake chakula, na kuwagawia kazi watumishi wake. Hufikiria kununua shamba, kisha hulinunua, na kulima zabibu kwa faida ya jasho lake. Huwa tayari kufanya kazi kwa nguvu na kuiimarisha mikono yake. Hutambua kwamba shughuli zake zina faida; hufanya kazi hata usiku kwa mwanga wa taa yake. Husokota nyuzi kwa mikono yake mwenyewe, kwa vidole vyake mwenyewe husuka nguo zake. Huufungua mkono wake kuwapa maskini, hunyosha mkono kuwasaidia fukara. Hawahofii watu wake ijapo baridi ya kipupwe, maana kila mmoja anazo nguo za kutosha. Hujitengenezea matandiko, mavazi yake ni ya zambarau ya kitani safi. Mume wake ni mtu mashuhuri barazani, anakoshiriki vikao vya wazee wa nchi. Mwanamke huyo hutengeneza nguo na kuziuza, huwauzia wafanyabiashara mishipi. Nguvu na heshima ndizo sifa zake, hucheka afikiriapo wakati ujao. Hufungua kinywa kunena kwa hekima, huwashauri wengine kwa wema. Huchunguza yote yanayofanyika nyumbani mwake, kamwe hakai bure hata kidogo. Watoto wake huamka na kumshukuru, mumewe huimba sifa zake. Husema, “Wanawake wengi wametenda mambo ya ajabu, lakini wewe umewashinda wote.” Madaha huhadaa na uzuri haufai, bali mwanamke amchaye Mwenyezi-Mungu atasifiwa. Jasho lake lastahili kulipwa, shughuli zake hazina budi kuheshimiwa popote. Yafuatayo ni maneno ya Mhubiri mwana wa Daudi, aliyekuwa mfalme huko Yerusalemu. Bure kabisa, bure kabisa, nakuambia mimi Mhubiri! Kila kitu ni bure kabisa! Binadamu hufaidi nini kwa jasho lake lote hapa duniani? Kizazi chapita na kingine chaja, lakini dunia yadumu daima. Jua lachomoza na kutua; laharakisha kwenda machweoni. Upepo wavuma kusini, wazunguka hadi kaskazini. Wavuma na kuvuma tena, warudia mzunguko wake daima. Mito yote hutiririkia baharini, lakini bahari kamwe haijai; huko ambako mito hutiririkia ndiko huko inakotoka tena. Mambo yote husababisha uchovu, uchovu mkubwa usioelezeka. Jicho halichoki kuona, wala sikio kusikia. Yaliyokuwako ndio yatakayokuwako, yaliyotendeka ndio yatakayotendeka; duniani hakuna jambo jipya. Watu husema, “Tazama jambo jipya,” kumbe lilikwisha kuwako zama za kale. Hakuna mtu anayekumbuka ya zamani wala atakayekumbuka yatakayotukia baadaye. Mimi Mhubiri, nilikuwa mfalme wa Israeli, huko Yerusalemu. Nilipania kuchunguza na kutafuta kwa hekima kila kitu kinachotukia duniani. Hiyo ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu. Nimeyaona yote yanayofanywa duniani; yote ni bure: Ni sawa na kufukuza upepo! Kilichopindika hakiwezi kunyoshwa, kisichokuwapo hakiwezi kuhesabiwa. Basi, nikatafakari nikisema, “Nimejipatia hekima nyingi zaidi kupita wote waliopata kutawala Yerusalemu kabla yangu. Naam, nina uzoefu wa hekima na maarifa.” Nilipania kubainisha kati ya hekima, wazimu na upumbavu. Lakini niligundua kwamba kufanya hivyo ni sawa na kufukuza upepo. Maana katika kuwa na hekima nyingi mna wasiwasi; na aongezaye maarifa zaidi huongeza huzuni zaidi. Basi, nikawaza; “Ngoja nijitumbukize katika starehe, nijifurahishe.” Lakini, niligundua kwamba kufanya hivyo ni bure kabisa. Nikasema kuhusu kicheko, “Ni wazimu”, na starehe “Mna faida gani?” Nilifikiria sana, namna ya kujichangamsha akili kwa divai, huku nikisukumwa na ari yangu ya kupata hekima; pia namna ya kuandamana na upumbavu ili nione yaliyo bora kabisa ambayo wanadamu wanaweza wakafanya waishipo maisha yao mafupi hapa duniani. Nilifanya mambo makuu: Nilijenga majumba na kujilimia mashamba ya mizabibu. Nilijifanyia bustani na viunga, nikapanda miti ya matunda ya kila aina. Nilijichimbia mabwawa ya maji ya kumwagilia hiyo miti. Nilinunua watumwa, wanawake kwa wanaume, na wengine wakazaliwa nyumbani mwangu. Nilikuwa na mali nyingi, makundi ya ng'ombe na kondoo wengi kuliko mtu yeyote aliyenitangulia kukaa Yerusalemu. Nilijirundikia fedha na dhahabu kutoka hazina za wafalme na toka mikoani, nami nilipata waimbaji wanaume kwa wanawake, na masuria watamaniwao. Naam, nikawa mkuu, mkuu kuwapita wote waliopata kuwako Yerusalemu kabla yangu; na hekima yangu ikakaa ndani mwangu. Kila macho yangu yalichokitamani nilikipata. Moyo wangu sikuunyima raha yoyote ile; kwa kuwa moyo wangu ulifurahia niliyotenda, na hili lilikuwa tuzo la jasho langu. Kisha nikafikiria yote niliyokuwa nimefanya kwa mikono yangu, jinsi nilivyotoa jasho katika kufanya hayo. Nikagundua kwamba yote yalikuwa bure kabisa; ilikuwa ni sawa na kufukuza upepo, hapakuwapo faida yoyote chini ya mbingu. Basi, nikaanza kufikiria maana ya kuwa na hekima, kuwa mwendawazimu, na kuwa mpumbavu. Nilijiuliza, “Mtawala mpya anaweza kufanya kitu gani?” Basi, mimi nikagundua kwamba hekima ni bora kuliko upumbavu, kama mwanga ulivyo bora kuliko giza. Mwenye hekima anayo macho, huona aendako, lakini mpumbavu hutembea gizani. Hata hivyo, nikatambua kwamba mwenye hekima na mpumbavu mwisho wao ni uleule. Basi, nikasema moyoni mwangu, “Yatakayompata mpumbavu yatanipata na mimi pia. Kwa nini, basi, nimekuwa na hekima kiasi chote hiki?” Nikajibu, nikiwaza, “Hayo nayo ni bure kabisa.” Maana hakuna amkumbukaye mwenye hekima, wala amkumbukaye mpumbavu, kwani siku zijazo wote watasahaulika. Jinsi mwenye hekima afavyo ndivyo afavyo mpumbavu! Kwa hiyo, nikayachukia maisha, maana yote yatendekayo duniani yalinisikitisha. Yote yalikuwa bure kabisa; nilikuwa nikifukuza upepo. Nilichukia kazi yangu yote niliyokuwa nimefanya hapa duniani, kuona kwamba ilinipasa nimwachie mtu ambaye atatawala baada yangu. Tena, ni nani ajuaye kwamba atakuwa mwenye hekima au atakuwa mpumbavu? Hata hivyo, yeye atamiliki yote niliyofanya kwa kutumia hekima yangu hapa duniani. Pia hayo yote ni bure kabisa. Basi, nilipofikiria tena juu ya yote niliyofanya duniani, nilikata tamaa. Maana, wakati mwingine mtu ambaye amefanya kazi kwa kutumia hekima, akili na maarifa yake, humwachia mtu mwingine afurahie matunda ya kazi ambayo hakuitolea jasho. Pia hilo nalo ni bure kabisa; ni jambo baya sana. Mtu anafaidi nini kutokana na kazi zake zote, na juhudi anazohangaika nazo duniani? Kwa sababu maisha yake yote yamejaa taabu, na kazi yake ni mahangaiko matupu; hata usiku akili yake haipumziki! Hayo nayo ni bure kabisa. Hakuna chema kimfaacho binadamu, isipokuwa kula na kunywa na kuifurahia kazi yake. Hili nalo nimeliona kuwa latoka kwa Mungu, maana usipojaliwa na Mungu, huwezi kupata chakula wala kujifurahisha. Mungu humjalia mtu apendezwaye naye hekima, akili na furaha; lakini humpa mwenye dhambi kazi ya kuvuna na kurundika, kisha akampa anayempendeza yeye Mungu. Yote hayo pia ni bure kabisa; ni sawa na kufukuza upepo. Kila kitu kina majira yake, kila jambo duniani lina wakati wake: Wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa; wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna kilichopandwa; wakati wa kuua na wakati wa kuponya; wakati wa kubomoa na wakati wa kujenga; wakati wa kulia na wakati wa kucheka; wakati wa kuomboleza na wakati wa kucheza; wakati wa kutupa mawe na wakati wa kuyakusanya mawe pamoja; wakati wa kukumbatia na wakati wa kuacha kukumbatia; wakati wa kutafuta na wakati wa kupoteza; wakati wa kuhifadhi na wakati wa kutupa; wakati wa kurarua na wakati wa kushona; wakati wa kukaa kimya na wakati wa kuongea; wakati wa kupenda na wakati wa kuchukia; wakati wa vita na wakati wa amani. Mfanyakazi hufaidi nini kutokana na juhudi zake hizo? Mimi nimeiona kazi ambayo binadamu amepewa na Mungu. Mungu amekifanya kila kitu kiwe kizuri kwa wakati wake. Amempa binadamu hamu ya kujua mambo ya baadaye, lakini hajamjalia fursa ya kuelewa matendo yake Mungu tangu mwanzo mpaka mwisho. Najua kwamba, kwa binadamu, liko jambo moja tu la kumfaa; kufurahi na kujifurahisha muda wote aishipo. Sote inatupasa kula na kunywa na kufurahia matunda ya kazi zetu. Hayo ni majaliwa ya Mungu. Najua kwamba lolote atendalo Mungu linadumu milele. Hakuna kinachoweza kuongezwa wala kupunguzwa; Mungu amefanya mambo yawe hivyo kusudi wanadamu wamche yeye. Kinachotukia sasa, kilikwisha tukia; kitakachotukia baadaye kilikwisha tukia; na Mungu hukifanya kitu kilekile kitukie tena na tena. Zaidi ya hayo, nimegundua duniani kwamba, mahali pa haki na uadilifu, uovu unatawala. Basi, nikasema moyoni mwangu, “Haidhuru! Mungu atawahukumu waadilifu, hali kadhalika na waovu, maana amepanga wakati maalumu kwa kila jambo na kwa kila kazi.” Nikasema moyoni mwangu, “Mungu anawajaribu binadamu, ili kuwaonesha kwamba wao ni sawa tu na wanyama.” Mwisho wa binadamu na mwisho wa mnyama ni uleule. Jinsi anavyokufa binadamu ndivyo anavyokufa mnyama. Wote hupumua namna ileile; binadamu si bora kuliko mnyama. Kwao yote ni bure kabisa. Wote hufa na kwenda mahali pamoja. Wote wametoka mavumbini; na wote watarudi mavumbini, Nani ajuaye, basi, kama kweli roho ya mtu hupaa juu, na roho ya mnyama hudidimia chini ardhini? Ndipo nikatambua kwamba hakuna jambo lililo bora zaidi kwa binadamu kufanya kuliko kufurahia kazi yake, kwa sababu amepangiwa hivyo. Nani awezaye kumjulisha binadamu yale yatakayokuwa baada ya kufa kwake? Kisha nikaona udhalimu wote unaofanyika duniani. Watu wanaokandamizwa hulia machozi, lakini hakuna yeyote anayewafariji. Wakandamizaji wao wana nguvu, ndiyo sababu hakuna wa kuwafariji. Basi, nikafikiri moyoni kuwa wafu waliokwenda wasikorudi, wana nafuu zaidi kuliko watu walio hai. Lakini ana heri zaidi kuliko wafu na walio hai, yule ambaye bado hajazaliwa na kuona maovu yote yanayotendwa hapa duniani. Tena niligundua kwamba juhudi zote za mtu na ujuzi wake katika kazi vyatokana na kuoneana wivu. Hayo nayo ni bure kabisa; ni sawa na kufukuza upepo. Mpumbavu hafanyi kazi na mwisho hujiua kwa njaa. Ni afadhali kuwa na kidogo tu, pamoja na amani moyoni, kuliko kuwa na mengi, pamoja na taabu; sawa tu na kufukuza upepo. Tena, niliona jambo moja bure kabisa duniani. Nilimwona mtu mmoja asiye na mwana wala ndugu; hata hivyo, haachi kufanya kazi; hatosheki kamwe na mali yake; wala hatulii na kujiuliza: “Ninamfanyia nani kazi na kujinyima starehe?” Hilo nalo ni bure kabisa; ni shughuli inayosikitisha. Ni afadhali kuwa wawili kuliko mtu kuwa peke yake. Kwa sababu wawili watapata tuzo la kazi yao. Ikijatokea mmoja akaanguka, huyo mwenzake atamwinua. Lakini ole wake aliye peke yake akianguka! Huyo hatakuwa na mtu wa kumwinua! Hali kadhalika, wawili wakilala pamoja watapata joto; lakini mtu akiwa peke yake atajipatiaje joto? Mtu akiwa peke yake aweza kushindwa na adui, lakini wakiwa wawili watamkabili na kumshinda adui. Kamba tatu zikisokotwa pamoja hazikatiki kwa urahisi. Afadhali kijana maskini mwenye hekima kuliko mfalme mzee mpumbavu, ambaye hasikilizi shauri jema; hata ikiwa alikuwa mfungwa na sasa ni mfalme, au alizaliwa maskini na sasa ni mfalme. Niliwaona watu wote waishio duniani, hata yule kijana ambaye angechukua nafasi ya mfalme. Idadi ya watu haikuwa na kikomo, naye aliwatawala wote. Hata hivyo, wale wanaozaliwa baadaye hawatamfurahia. Hakika hayo nayo ni bure kabisa na kufukuza upepo. Uwe mwangalifu uendapo katika nyumba ya Mungu, na kukaribia ili kusikiliza kwa makini kuliko kutambika kama watambikavyo wapumbavu, watu wasiopambanua kati ya jema na ovu. Fikiri kabla ya kusema, wala usiwe mwepesi kusema chochote mbele ya Mungu, kwa maana Mungu yuko mbinguni na wewe uko duniani. Kwa hiyo usiseme mengi. Kadiri mtu anavyohangaika zaidi, ndivyo atakavyoota ndoto; sauti ya mpumbavu ni maneno mengi. Ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuitimiza; na Mungu hapendezwi na wapumbavu. Tekeleza ulichoahidi. Ni afadhali kutoweka nadhiri kuliko kuweka nadhiri kisha usiitimize. Angalia mdomo wako usikuingize dhambini, halafu ikupase kumwambia mjumbe wa Mungu kwamba hukunuia kutenda dhambi. Ya nini kumfanya Mungu akukasirikie na kuiharibu kazi yako? Ndoto zikizidi, kuna maangamizi na maneno huwa mengi. Jambo la maana ni kumcha Mungu. Usishangae ukiona katika nchi watu fukara wanakandamizwa, wananyimwa haki zao na maslahi yao. Kila mwenye cheo anayewadhulumu wanyonge yupo chini ya mkuu mwingine, na juu ya hao wote kuna wakuu zaidi. Hata hivyo, mfalme akijishughulisha na kilimo ni manufaa kwa wananchi wote. Apendaye fedha hatatosheka na fedha; wala atamaniye mali hata akiipata hatatosheka. Hilo nalo ni bure kabisa. Ongezeko la mali huleta ongezeko la walaji, naye mwenye mali yamfaa nini isipokuwa kuitazama tu mali yake? Usingizi wa kibarua ni mtamu, awe ameshiba au amekula kidogo tu. Lakini usingizi wa tajiri ni wa wasiwasi daima, maana ziada ya mali yake humsumbua usiku kucha. Tena, nimeona jambo moja ovu sana duniani: Mtu alijirundikia mali ikawa hatari kwake. Kwa bahati mbaya, mali hiyo iliharibiwa katika matumizi mabaya, mwisho, mtu huyo hakuwa na chochote mkononi na alikuwa na mwana. Kama vile binadamu alivyokuja duniani uchi toka tumboni mwa mama yake, ndivyo atakavyorudi uchi huko alikotoka. Hataweza kuchukua hata sehemu ndogo ya mapato ya kazi yake. Hili nalo ni jambo baya sana. Atarudi kama alivyokuja. Amejisumbua kufukuza upepo, akatoka jasho bure. Aliishi maisha yake yote katika giza na huzuni; katika mahangaiko, magonjwa na hasira. Basi, haya ndiyo niliyogundua: Jambo zuri na la kufaa kwa binadamu ni kula, kunywa na kufurahia matunda ya jasho analotoa katika kazi anayoifanya hapa duniani, siku hizo chache za maisha aliyojaliwa na Mungu, maana hivyo ndivyo alivyopangiwa. Kama Mungu anampa mtu utajiri na mali na kumjalia fursa ya kufurahia hayo, basi binadamu ashukuru na avifaidi hivyo alivyojipatia kwa jasho lake. Hiyo ni zawadi kutoka kwa Mungu. Na kwa kuwa Mungu amemruhusu kuwa na furaha, binadamu hatakuwa na wasiwasi mwingi juu ya maisha yake mafupi. Nimeona jambo moja ovu hapa duniani, linalowakandamiza watu: Mungu humjalia mtu utajiri, mali na heshima, asitindikiwe kitu chochote anachotamani, lakini hampi uwezo wa kuvifurahia vitu hivyo; badala yake, mgeni fulani atavifaidi. Hilo nalo ni bure kabisa; ni jambo la mateso makali. Mtu akiweza kuzaa watoto 100, na akaishi maisha marefu, lakini kama mtu huyo hafurahii maisha yake, wala hafanyiwi mazishi basi nasema mtoto aliyezaliwa amekufa ni afadhali kuliko mtu huyo. Mtoto mfu hafaidiki chochote kwa kuzaliwa; yeye hutokomea gizani, akasahaulika. Zaidi ya hayo, mtoto wa namna hiyo hakupata kuuona mwanga wa jua wala kutambua chochote. Hata hivyo, huyo mtoto angalau hupata pumziko ambapo yule mtu hapati. Ingawa mtu huyo ataishi miaka elfu mbili, lakini hafurahii maisha, basi ni kama huyo mtoto wote wawili huenda mahali pamoja. Kazi yote ya mtu ni kwa ajili ya kupata chakula, lakini tamaa yake ya kula haitoshelezwi kamwe. Je, mtu mwenye hekima anayo nafuu zaidi kuliko mpumbavu? Na mtu maskini hupata faida gani akijua namna ya kuyakabili maisha? Hayo nayo ni bure kabisa; ni sawa na kufukuza upepo. Afadhali kuridhika na ulicho nacho kuliko kuhangaika kwa kutamani kitu kingine. Kila kitu kinachotukia kilikwisha pangwa hapo awali; hali ya binadamu inajulikana, na tunajua kwamba mnyonge hawezi kubishana na mtu mwenye nguvu zaidi. Maneno mengi hayana faida, hayamwinui binadamu. Nani ajuaye yamfaayo mtu katika maisha haya mafupi yasiyo na faida, maisha ambayo hupita kama kivuli? Nani duniani ajuaye yatakayompata mtu baada ya kufa? Sifa njema ni bora kuliko marashi ya thamani. Siku ya kufa ni bora kuliko siku ya kuzaliwa. Afadhali kwenda kwenye matanga, kuliko kwenda kwenye karamu, kwa sababu walio hai yawapasa kukumbuka kwamba kifo chatungojea sisi sote. Huzuni ni afadhali kuliko kicheko maana, huzuni ya uso ni faida ya moyo. Moyo wa mwenye hekima huthamini matanga, lakini moyo wa mpumbavu hupenda raha. Afadhali kusikia maonyo ya wenye hekima kuliko kusikiliza nyimbo za wapumbavu. Maana, kicheko cha mpumbavu ni kama mlio wa miiba motoni. Hayo nayo ni bure kabisa. Mwenye hekima akimdhulumu mtu; hujifanya mwenyewe kuwa mpumbavu kupokea rushwa hupotosha akili. Mwisho wa jambo ni afadhali kuliko mwanzo wake; mvumilivu rohoni ni bora kuliko mwenye majivuno. Usiwe mwepesi wa hasira, maana, hasira hukaa ndani ya wapumbavu. Usiulize, “Kwa nini nyakati za kale zilikuwa bora kuliko za sasa?” Huulizi hivyo kwa kutumia hekima. Hekima ni ya thamani kubwa kama urithi; ni muhimu kwa wale wote walio hai. Kulindwa na hekima ni kama kulindwa na fedha. Faida ya maarifa ni kwamba hekima hulinda maisha ya mtu aliye nayo. Tafakarini vema kazi yake Mungu; ni nani awezaye kunyosha alichopinda Mungu? Katika siku za fanaka uwe na furaha; katika siku za maafa utafakari jambo hili: Fanaka, pia maafa, Mungu amefanya hiyo ya kwanza iambatane na ya pili ili binadamu asiweze kujua yatakayotukia baada yake. Katika maisha yangu duni, nimeona kila kitu; mtu mwadilifu hufa ingawa ni mwadilifu, ambapo mtu mwovu huendelea kuishi maisha marefu ingawa ni mwovu. Basi, usiwe mwadilifu sana, wala usiwe mwenye hekima mno! Ya nini kujiangamiza wewe mwenyewe? Lakini pia, usiwe mwovu sana wala usiwe mpumbavu! Ya nini kufa kabla ya wakati wako? Inakupasa ushike la kwanza na la pili pia; maana anayemtii Mungu atajengwa kwayo. Hekima humfanya mwenye busara kuwa na nguvu zaidi kuliko watawala kumi mjini. Hakika, hakuna mtu mwadilifu duniani atendaye mema daima bila kutenda dhambi. Usitie maanani maneno yote wasemayo wanadamu, usije ukamsikia mtumishi wako akikutukana. Wewe mwenyewe wajua moyoni kwamba umeapiza wengine mara nyingi. Nimeyapima hayo yote kwa hekima; nikajisemea: “Nataka kuwa mwenye hekima!” Lakini hekima iko mbali sana nami. Jinsi gani binadamu ataweza kugundua maana ya maisha; jambo hilo ni zito na gumu mno kwetu! Hata hivyo, nilipania kujua na kuchunguza na kutafuta hekima na maana ya mambo yaliyoko, na pia kujua uovu ni upuuzi, na upumbavu ni wazimu. Jambo moja nililogundua lililo baya zaidi kuliko kifo, ni mwanamke ambaye moyo wake ni mtego na wavu, na mikono yake ni kama minyororo. Lakini anayempendeza Mungu humkwepa mwanamke huyo, lakini mwenye dhambi hunaswa naye. Haya, nakuambia mimi Mhubiri, ndio niliyogundua nilipofanya uchunguzi wangu kidogokidogo. Nilipania kugundua mambo hayo tena na tena, lakini sikufaulu. Kati ya wanaume elfu moja, nilifaulu kumwona mwanamume mmoja, anayestahili heshima, lakini kati ya wanawake wote kama hao sikumwona hata mmoja anayestahili heshima. Tazama, nimegundua jambo hili moja: Kwamba Mungu aliwaumba wanadamu wanyofu, lakini wao wenyewe wamejitafutia matatizo. Nani aliye kama mwenye hekima? Nani ajuaye hali halisi ya vitu? Hekima humletea mtu tabasamu, huubadilisha uso wake mwenye huzuni. Tii amri ya mfalme, kwa sababu ya kiapo chako kitakatifu. Usifanye haraka kuondoka mbele yake; wala usiwe na kiburi juu ya jambo baya, maana mfalme hufanya apendavyo. Amri ya mfalme ni kauli ya mwisho; nani athubutuye kumwuliza, “Unafanya nini?” Anayetii amri hatapata madhara, na mwenye hekima atajua kuna wakati na njia. Naam, kila kitu kina wakati wake na njia yake, ingawa binadamu anakabiliwa na tatizo kubwa: Hajui ni nini kitakachotukia baadaye, kwani nani awezaye kumjulisha yatakayotukia baadaye? Hakuna mtu aliye na uwezo wa kushikilia roho yake asife; hakuna mtu aliye na uwezo juu ya siku ya kufa. Wakati wa vita hakuna kuponyoka, na uovu hauwezi kumwokoa mwovu. Haya yote nimeyaona katika uchunguzi wangu juu ya yote yanayotendwa hapa duniani, binadamu anapokuwa na uwezo wa kumkandamiza na kumdhuru binadamu mwenzake. Tena, nimewaona waovu wakizikwa, na watu waliporudi kutoka mahali patakatifu wanawasifu humohumo mjini walimotenda maovu yao. Hayo nayo ni bure kabisa. Kwa vile uovu haupatilizwi haraka, mioyo ya wanadamu hupania kutenda mabaya. Wenye dhambi hutenda maovu mara mia, hata hivyo, huendelea kuishi. Walakini, mimi najua kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, kwa sababu ya uchaji wao; lakini hakuna furaha kwa waovu. Wao watapita kama kivuli, maisha yao hayatakuwa marefu kwa sababu hawamchi Mungu. Kuna jambo moja, bure kabisa nililoligundua hapa duniani: Watu wema hutendewa wastahilivyo waovu, nao waovu hutendewa wastahilivyo watu wema. Hili nalo nasema ni bure kabisa. Basi, mimi nasisitiza kuwa mtu ni lazima afaidi raha, kwa kuwa hapa duniani hakuna kilicho kizuri zaidi kuliko kula na kunywa na kujifurahisha. Hayo ndio awezayo kufanya mtu anaposhughulika na kazi katika muda wa maisha yake aliyojaliwa na Mungu duniani. Kila nilipojaribu kujua hekima na kuona yanayotendeka hapa duniani, niligundua kwamba unaweza kukaa macho mchana na usiku, halafu niliona kazi yote ya Mungu ya kwamba mwanadamu hawezi kuelewa kazi inayofanyika duniani. Wenye hekima wanaweza kujidai eti wanajua, lakini, kwa kweli, hawajui. Nilitafakari juu ya hayo yote, nikaona kwamba Mungu anaongoza matendo ya watu wenye hekima na waadilifu; ikiwa ni upendo au chuki, binadamu hajui. Kila kitu kwao ni bure kabisa, maana mwisho uleule huwapata waadilifu na waovu, wema na wabaya, walio safi na walio najisi, wenye kutoa sadaka na wasiotoa sadaka. Aliye mwema ni sawa tu na mwenye dhambi, na mwenye kuapa si tofauti na asiyeapa. Hili ni jambo baya zaidi kati ya yote yatukiayo hapa duniani, kwamba mwisho uleule huwapata wote. Tena, wakati wote wa maisha yao, wanadamu huwa wamejaa uovu na wazimu, na kisha hufa. Lakini anayeambatana na walio hai analo bado tumaini, afadhali mbwa hai kuliko simba mfu. Maana, walio hai hujua ya kwamba watakufa, lakini wafu hawajui chochote. Hawana tuzo tena; hata kumbukumbu lao limesahauliwa kabisa. Upendo wao, chuki zao na tamaa zao, vyote vimetoweka pamoja nao, na wala hawatashiriki chochote hapa duniani. Nenda ukale chakula chako kwa furaha, ukanywe na divai yako kwa moyo mchangamfu, maana Mungu amekwisha ikubali kazi yako. Vaa vizuri, jipake mafuta kichwani. Furahia maisha pamoja na mke wako umpendaye muda wote wa maisha yako ya bure ambayo Mungu amekujalia hapa duniani; maana hilo ndilo ulilopangiwa maishani, katika kazi zako hapa duniani. Kila unachotaka kufanya kifanye kwa nguvu zako zote, maana, hakuna kazi, wala wazo, wala maarifa, wala hekima huko kuzimu unakokwenda. Tena, nimeona kitu kimoja hapa duniani, kwamba wenye mbio hawafaulu katika riadha, wala wenye nguvu hawashindi vita; wenye busara hawapati chakula, wenye akili hawatajiriki, wala wenye ujuzi hawapandi vyeo; lakini wakati wa bahati huwapata wote pamoja. Mtu hajui saa yake itafika lini. Kama vile samaki wanavyonaswa katika wavu kwa bahati mbaya, na kama vile ndege wanavyonaswa katika mtego kwa ghafla, ndivyo wanadamu wanavyonaswa na balaa inapowaangukia bila ya kutazamia. Pia hapa duniani nimeona mfano wa hekima, na ulionekana kwangu kuwa wenye maana sana. Palikuwa na mji mmoja mdogo wenye wakazi wachache. Mfalme mmoja mwenye nguvu akafika, akauzingira na kujiandaa kuushambulia. Katika mji huo, alikuwapo maskini mmoja mwenye hekima, ambaye, kwa hekima yake aliuokoa mji huo. Lakini hakuna mtu aliyemkumbuka huyo maskini baadaye. Basi, mimi nasema, hekima ni bora kuliko nguvu, ingawa hekima ya maskini haithaminiwi, na maneno yake hayasikilizwi. Afadhali kusikiliza maneno matulivu ya mwenye hekima, kuliko kusikiliza kelele za mfalme katika kikao cha wapumbavu. Kuwa na hekima ni bora kuliko kutegemea silaha, lakini mwenye dhambi mmoja huharibu mazuri mengi. Nzi waliokufa husababisha marashi kunuka; upumbavu kidogo hubatilisha hekima na heshima. Moyo wa mwenye hekima humwongoza kutenda yaliyo sawa; lakini mtu mpumbavu moyo wake humpotosha. Hata apitapo njiani, mpumbavu hutambulikana hivyo, humjulisha kila mtu kwamba yeye ni mpumbavu. Mtawala akikuwakia hasira, usijiuzulu; makosa makubwa huweza kufutwa ukiwa mnyenyekevu. Kuna uovu niliogundua hapa duniani, uovu unaosababishwa na watawala: Kwamba wapumbavu wanapewa kazi za madaraka ya juu, na matajiri wanachukua nafasi za mwisho. Nimeona watumwa wanapanda farasi, na wakuu wanatembea kwa miguu kama watumwa. Mchimba shimo hutumbukia mwenyewe, abomoaye ukuta huumwa na nyoka. Mchonga mawe huumizwa nayo, mkata kuni hukabiliwa na hatari. Nguvu nyingi zaidi zahitajika kwa mtumiaji shoka butu lisilonolewa, lakini kutumia hekima humfanya mtu afanikiwe. Nyoka akiuma kabla hajachochewa, mchochezi hahitajiki tena. Maneno ya mwenye hekima humnufaisha asemaye; lakini midomo ya mpumbavu humwangamiza. Mpumbavu huanza kusema kwa maneno ya kijinga, na kumaliza kauli yake kwa wazimu mbaya. Mpumbavu hububujika maneno. Binadamu hajui yatakayokuwako, wala yale yatakayotukia baada yake. Mpumbavu huchoshwa na kazi yake hata asijue njia ya kurudia nyumbani. Ole wako, ewe nchi, mtawala wako akiwa kijana, na viongozi wako wakifanya sherehe asubuhi. Heri yako, ewe nchi, mtawala wako akiwa mtu wa heshima, na viongozi wako wakifanya sherehe wakati wa kufaa, ili kujipatia nguvu na si kujilewesha. Kutokana na uvivu wa mtu, paa hubonyea; kwa sababu ya uzembe, nyumba huvuja. Chakula ni kwa ajili ya kujifurahisha, divai huchangamsha maisha; na fedha husababisha hayo yote. Usimwapize mtawala hata moyoni mwako, wala usimwapize tajiri hata chumbani mwako unakolala, kwa kuwa ndege ataisikia sauti yako, au kiumbe arukaye atatangaza maneno yako. Jishughulishe na biashara hata kama kwa kubahatisha; yawezekana baadaye ukapata chochote kile. Wagawie watu saba hata wanane sehemu yako, maana, hujui balaa litakalofika duniani. Mawingu yakijaa maji, mvua hunyesha; mti ukiangukia kusini au kaskazini, hapo uangukiapo ndipo ulalapo. Anayengoja upepo hatapanda mbegu, anayesubiri mawingu yatoweke, hatavuna kitu. Usivyojua jinsi uhai unavyoingia katika mifupa ya mtoto tumboni mwa mamake, kadhalika huwezi kuelewa matendo ya Mungu, ambayo hufanya kila kitu. Panda mbegu asubuhi na jioni usiache kupanda, maana, hujui zipi zitaota; za asubuhi, za jioni, au zote zitakuwa nzuri. Mwanga wafaa, na kuliona jua kwapendeza macho. Mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie miaka hiyo yote; lakini akumbuke kuwa siku za giza zitakuwa nyingi, na kwamba yote yatakayofuata ni bure. Ewe kijana, furahia ujana wako, moyo wako, uchangamke wakati ungali kijana. Fuata mapenzi ya moyo wako na upeo wa macho yako. Lakini kumbuka kwamba Mungu atakuhukumu kadiri ya hayo yote. Ondoa mahangaiko moyoni mwako, jikinge, usipate maumivu mwilini kwa sababu ujana na mwisho wa maisha ni bure kabisa. Umkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku na miaka ambapo utasema: “Sifurahii tena vitu hivyo!” Umkumbuke kabla ya wakati ambapo kwako mwanga wa jua utafifia; mwezi na nyota haviangazi tena, nayo mawingu yametanda tena baada ya mvua. Wakati ambapo mikono inayokulinda inatetemeka, miguu yako imara imepindika, meno yako ya kusagia hayafai kwa uchache, na macho ya kuchungulia dirishani yamefifia. Wakati ambapo milango ya masikio yako imezibika, na sauti za visagio ni hafifu; lakini usiku hata kwa sauti ya ndege utagutuka. Wakati huo utaogopa kupanda mahali pa juu na kutembea barabarani ni kitisho; wakati miti ya mlozi inachanua na panzi wanashiba, lakini wewe hutakuwa na hamu tena. Wakati huo binadamu anapaswa kwenda katika makao yake ya milele, nao waombolezaji watapitapita barabarani. Wakati huo uzi wa dhahabu utakatika, bakuli la dhahabu litapasuka, mtungi wa maji utavunjikia kisimani, kadhalika na gurudumu la kuvutia maji. Nawe vumbi utarudia udongoni ulimotolewa na roho yako itamrudia Mungu aliyeiumba. Mimi Mhubiri nasema: Yote ni bure kabisa! Yote ni bure. Basi, zaidi ya kuwa na hekima yake, Mhubiri aliwafundisha watu ujuzi. Alizipima, akazichunguza na kuzirekebisha methali kwa ustadi mwingi. Mhubiri alijitahidi kupata maneno ya kupendeza, akaandika kwa ufasaha maneno ya kweli. Misemo ya wenye hekima ni kama michokoo na methali zilizokusanywa pamoja na mchungaji mmoja ni kama vigingi vilivyopigiliwa imara ardhini. Zaidi ya hayo, mwanangu, jihadhari! Kuandika vitabu hakuna mwisho na kusoma kwingi huchokesha mwili. Baada ya hayo yote yaliyokwisha semwa bado kuna hili linalotakiwa: Mche Mungu, na uzishike amri zake; kwa sababu hilo ndilo jukumu aliloumbiwa binadamu. Maana, Mungu atahukumu matendo yetu yote, hata yale yanayotendwa kwa siri, yawe mema au mabaya. Wimbo wa Solomoni ulio bora kuliko nyimbo zote. Heri midomo yako inibusu, maana pendo lako ni bora kuliko divai. Manukato yako yanukia vizuri, na jina lako ni kama marashi yaliyomiminwa. Kwa hiyo wanawake hukupenda! Nichukue, twende zetu haraka, mfalme amenileta katika chumba chake. Tutafurahi na kushangilia kwa sababu yako, tutasifu mapenzi yako kuliko divai. Wanawake wana haki kukupenda! Enyi wanawake wa Yerusalemu, mimi ni mweusi na ninapendeza, kama mahema ya Kedari, kama mapazia ya Solomoni. Msinishangae kwa sababu ni mweusi, maana jua limenichoma. Ndugu zangu walinikasirikia, wakanifanya mlinzi wa mashamba ya mizabibu. Lakini sikutunza shamba langu la mizabibu. Hebu niambie ee wangu wa moyo, utawalisha wapi kondoo wako? Ni wapi watakapopumzikia adhuhuri? Kwa nini mimi nikutafute kati ya makundi ya wenzako? Ewe upendezaye kuliko wanawake wote; kama hujui, fanya hivi: Zifuate nyayo za kondoo; basi, walishe mbuzi wako karibu na hema za wachungaji. Wewe ee mpenzi wangu, nakulinganisha na farasi dume wa magari ya Farao. Mashavu yako yavutia kwa vipuli, na shingo yako kwa mikufu ya johari. Lakini tutakufanyizia mikufu ya dhahabu, iliyopambwa barabara kwa fedha. Mfalme alipokuwa kwenye kochi lake, marashi yangu ya nardo yalisambaa kila mahali. Mpenzi wangu ni kama mfuko wa manemane kwangu, kati ya matiti yangu. Mpenzi wangu ni kama maua ya hina yachanuayo, kwenye mashamba ya mizabibu huko Engedi. Hakika u mzuri, ee mpenzi wangu, hakika u mzuri! Macho yako ni kama ya hua! Hakika u mzuri ewe nikupendaye, u mzuri kweli! Majani mabichi yatakuwa kitanda chetu; mierezi itakuwa nguzo za nyumba yetu, na miberoshi itakuwa dari yake. Mimi ni ua la Sharoni, ni yungiyungi ya bondeni. Kama yungiyungi kati ya michongoma, ndivyo alivyo mpenzi wangu kati ya wasichana. Kama mtofaa kati ya miti ya msituni, ndivyo alivyo mpenzi wangu kati ya wavulana. Nafurahia kuketi chini ya kivuli chake, na tunda lake tamu sana kwangu. Alinichukua hadi ukumbi wa karamu, akatweka bendera ya mapenzi juu yangu. Nishibishe na zabibu kavu, niburudishe kwa matofaa, maana naugua kwa mapenzi! Mkono wake wa kushoto chini ya kichwa changu, mkono wake wa kulia wanikumbatia. Nawasihi enyi wanawake wa Yerusalemu, kama walivyo paa au swala wa porini, msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi, hadi hapo wakati wake utakapofika. Hiyo ni sauti ya mpenzi wangu, yuaja mbio, anaruka milima, vilima anavipita kasi! Mpenzi wangu ni kama paa, ni kama swala mchanga. Amesimama karibu na ukuta wetu, achungulia dirishani, atazama kimiani. Mpenzi wangu aniambia: “Inuka basi, ewe mpenzi wangu, unipendezaye, njoo twende zetu. Tazama, majira ya baridi yamepita, nazo mvua zimekwisha koma; maua yamechanua kila mahali. Wakati wa kuimba umefika; sauti ya hua yasikika mashambani mwetu. Mitini imeanza kuzaa; na mizabibu imechanua; inatoa harufu nzuri. Njoo, basi, ewe mpenzi wangu unipendezaye, njoo twende. Ee hua wangu, uliyejificha miambani. Hebu niuone uso wako, hebu niisikie sauti yako, maana sauti yako yapendeza na uso wako wavutia. “Tukamatieni mbweha, wale mbweha wadogowadogo, wanaoiharibu mizabibu yetu inayochanua.” Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake. Yeye hulisha kondoo wake penye yungiyungi, hadi hapo jua linapochomoza na vivuli kutoweka. Rudi kama paa mpenzi wangu, kama swala mdogo juu ya milima ya Betheri. Usiku nikiwa kitandani mwangu, niliota namtafuta nimpendaye moyoni mwangu; nilimtafuta, lakini sikumpata. Niliamka nikazunguka mjini, barabarani na hata vichochoroni, nikimtafuta yule wangu wa moyo. Nilimtafuta, lakini sikumpata. Walinzi wa mji waliniona walipokuwa wanazunguka mjini. Basi nikawauliza, “Je, mmemwona mpenzi wangu wa moyo?” Mara tu nilipoachana nao, nilimwona mpenzi wangu wa moyo; nikamshika wala sikumwachia aondoke, hadi nilipompeleka nyumbani kwa mama yangu, hadi chumbani kwake yule aliyenizaa. Nawasihini, enyi wanawake wa Yerusalemu, kama walivyo paa au swala, msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi, hadi hapo wakati wake utakapofika. Ni kitu gani kile kitokacho jangwani kama mnara wa moshi, kinukiacho manemane na ubani, manukato yauzwayo na wafanyabiashara? Tazama! Ni machela ya Solomoni; amebebwa juu ya kiti chake cha enzi; amezungukwa na walinzi sitini, mashujaa bora wa Israeli. Kila mmoja wao ameshika upanga, kila mmoja wao ni hodari wa vita. Kila mmoja ana upanga wake mkononi, tayari kumkabili adui usiku. Mfalme Solomoni alijitengenezea machela, kwa mbao nzuri kutoka Lebanoni. Nguzo zake zilitengenezwa kwa fedha; mgongo wake kwa dhahabu; mahali pa kukalia pamefunikwa vitambaa vya zambarau, walichoshona kwa upendo wanawake wa Yerusalemu, waliokishonea alama za upendo. Njoni basi enyi wanawake wa Siyoni, mkamwone mfalme Solomoni. Amevalia taji aliyovikwa na mama yake, siku alipofanya harusi yake, naam, siku ambayo moyo wake ulijaa furaha. Hakika u mzuri ewe mpenzi wangu, hakika u mzuri! Macho yako ni kama ya hua nyuma ya shela lako, nywele zako ni kama kundi la mbuzi washukao katika milima ya Gileadi. Meno yako ni kama kondoo majike waliokatwa manyoya wanaoteremka baada ya kuogeshwa. Kila mmoja amezaa mapacha, na hakuna yeyote aliyefiwa. Midomo yako ni kama utepe mwekundu, kinywa chako chavutia kweli. Nyuma ya shela lako, mashavu yako ni kama nusu mbili za komamanga. Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, uliojengwa ili kuhifadhia silaha, ambako zimetundikwa ngao elfu moja zote zikiwa za mashujaa. Matiti yako ni kama paa mapacha, ambao huchungwa penye yungiyungi. Nitakaa kwenye mlima wa manemane, na kwenye kilima cha ubani, hadi hapo kutakapopambazuka, na giza kutoweka. Tazama ulivyo mzuri ee mpenzi wangu, wewe huna kasoro yoyote. Njoo, bibiarusi wangu tuondoke Lebanoni; na tuiachilie mbali Lebanoni. Shuka toka kilele cha mlima Amana, toka kilele cha Seniri na Hermoni, toka mapango ya simba, toka milima ya chui. Umefurahisha moyo wangu, dada yangu, bi arusi, umefurahisha moyo wangu, kwa kunitupia jicho mara moja tu, na kwa huo mkufu wako shingoni. Dada yangu, bi arusi; pendo lako ni tamu ajabu. Ni bora kuliko divai, marashi yako yanukia kuliko viungo vyote. Midomo yako yadondosha asali, ee bibiarusi wangu; ulimi wako una asali na maziwa. Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ya Lebanoni. Dada yangu, naam, bi arusi, ni bustani iliyofichika, bustani iliyosetiriwa; chemchemi iliyotiwa mhuri. Machipukizi yako ni bustani ya mikomamanga pamoja na matunda bora kuliko yote, hina na nardo. Nardo na zafarani, mchai na mdalasini manemane na udi, na mimea mingineyo yenye harufu nzuri. U chemchemi ya bustani, kisima cha maji yaliyo hai, vijito vitiririkavyo kutoka Lebanoni. Vuma, ewe upepo wa kaskazi, njoo, ewe upepo wa kusi; vumeni juu ya bustani yangu, mlijaze anga kwa manukato yake. Mpenzi wangu na aje bustanini mwake, ale matunda yake bora kuliko yote. Naingia bustanini mwangu, dada yangu, bi arusi. Nakusanya manemane na viungo, nala sega langu la asali, nanywa divai yangu na maziwa yangu. Kuleni enyi marafiki, kunyweni; kunyweni sana wapendwa wangu. Nililala, lakini moyo wangu haukulala. Sauti ya mpenzi wangu anabisha hodi. “Nifungulie, dada yangu mpenzi wangu, bibiarusi wangu, hua wangu, usiye na kasoro. Kichwa changu kimelowa umande na nywele zangu manyunyu ya usiku.” Nimekwisha yavua mavazi yangu, nitayavaaje tena? Nimekwisha nawa miguu yangu, niichafueje tena? Hapo mpenzi wangu akaugusa mlango, moyo wangu ukajaa furaha. Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu. Mikono yangu imejaa manemane, na vidole vyangu vyadondosha manemane, nilipolishika komeo kufungua mlango. Nilimfungulia mlango mpenzi wangu, lakini kumbe, alikuwa amekwisha toweka. Moyo wangu ulifurahi alipokuwa akizungumza! Nilimtafuta, lakini sikumpata; nilimwita, lakini hakuniitikia. Walinzi wa mji waliniona, walipokuwa wanazunguka mjini; wakanipiga na kunijeruhi; nao walinzi wa lango wakaninyanganya shela langu. Nawasihini, enyi wanawake wa Yerusalemu, mkimwona mpenzi wangu, mwelezeni kwamba naugua kwa mapenzi! Ewe upendezaye kuliko wanawake wote! Kwani huyo mpenzi wako ana nini cha zaidi ya mpenzi mwingine, hata utusihi kwa moyo kiasi hicho? Mpenzi wangu ni mzuri na mwenye nguvu, mashuhuri miongoni mwa wanaume elfu kumi. Kichwa chake kizuri kama dhahabu safi, nywele zake ni za ukoka, nyeusi ti kama kunguru. Macho yake ni kama ya hua kandokando ya kijito, ni kama njiwa waliooga maziwa kando ya kijito. Mashavu yake ni kama matuta ya rihani kama bustani iliyojaa manukato na manemane. Midomo yake ni kama yungiyungi, imelowa manemane kwa wingi. Mikono yake imewekwa bangili za dhahabu, amevalia johari za Tarshishi. Kiwiliwili chake ni kama pembe za ndovu zilizopambwa kwa vito vya johari ya rangi ya samawati. Miguu yake ni kama nguzo za alabasta zilizosimikwa katika misingi ya dhahabu. Umbo lake ni kama Lebanoni, ni bora kama miti ya mierezi. Kinywa chake kimejaa maneno matamu, kwa ujumla anapendeza. Basi, hivyo ndivyo alivyo mpenzi wangu, naam, ndivyo alivyo rafiki yangu, enyi wanawake wa Yerusalemu. Ewe mwanamke uliye mzuri sana; amekwenda wapi huyo mpenzi wako? Ameelekea wapi mpenzi wako ili tupate kushirikiana nawe katika kumtafuta? Mpenzi wangu amekwenda bustanini mwake, mahali ambapo rihani hustawi. Yeye analisha kondoo wake na kukusanya yungiyungi. Mimi ni wake mpenzi wangu, naye ni wangu; yeye huwalisha kondoo wake penye yungiyungi. Mpenzi wangu, wewe u mzuri kama Tirza, wapendeza kama Yerusalemu, unatisha kama jeshi lenye bendera. Hebu tazama kando tafadhali; ukinitazama nahangaika. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi, wateremkao chini ya milima ya Gileadi. Meno yako kama kundi la kondoo majike wanaoteremka baada ya kuogeshwa. Kila mmoja amezaa mapacha, na hakuna yeyote aliyefiwa. Mashavu yako ni kama nusu mbili za komamanga, nyuma ya shela lako. Wapo malkia sitini, masuria themanini, na wasichana wasiohesabika! Hua wangu, mzuri wangu, ni mmoja tu, na ni kipenzi cha mama yake; yeye ni wa pekee kwa mama yake. Wasichana humtazama na kumwita heri, nao malkia na masuria huziimba sifa zake. Nani huyu atazamaye kama pambazuko? Mzuri kama mwezi, mwangavu kama jua, na anatisha kama jeshi lenye bendera. Nimeingia katika bustani ya milozi kutazama machipuko ya bondeni, kuona kama mizabibu imechanua, na mikomamanga imechanua maua. Bila kutazamia, mpenzi wangu, akanitia katika gari la mkuu. Rudi, rudi ewe msichana wa Mshulami. Rudi, rudi tupate kukutazama. Mbona mwataka kunitazama miye Mshulami kana kwamba mnatazama ngoma kati ya majeshi mawili? Nyayo zako katika viatu zapendeza sana! Ewe mwanamwali wa kifalme. Mapaja yako ya mviringo ni kama johari, kazi ya msanii hodari. Kitovu chako ni kama bakuli lisilokosa divai iliyokolezwa. Tumbo lako ni kama lundo la ngano lililozungushiwa yungiyungi kandokando. Matiti yako ni kama paa mapacha, ni kama swala wawili. Shingo yako ni kama mnara wa pembe za ndovu; macho yako ni kama vidimbwi mjini Heshboni, karibu na mlango wa Beth-rabi. Pua yako ni kama mnara wa Lebanoni, ambao unauelekea mji wa Damasko. Kichwa chako juu yako ni kama mlima Karmeli, nywele zako za ukoka zangaa kama zambarau; uzuri wako waweza kumteka hata mfalme. Tazama ulivyo mzuri na wa kuvutia! Ewe mpenzi, mwali upendezaye! Umbo lako lapendeza kama mtende, matiti yako ni kama shada za tende. Nilisema nitaupanda mtende na kuzichuma shada za tende. Kwangu matiti yako ni kama shada za zabibu, harufu nzuri ya pumzi yako ni kama matofaa; na kinywa chako ni kama divai tamu. Basi divai na itiririke hadi kwa mpenzi wangu, ipite juu ya midomo yake na meno yake! Mimi ni wake mpenzi wangu, naye anionea sana shauku. Njoo ewe mpenzi wangu, twende mashambani, twende zetu tukalale huko vijijini. Tutaamka mapema, twende kwenye mashamba ya mizabibu, tukaone kama imeanza kuchipua, na kama maua ya zabibu yamekwisha kuchanua, pia kama mikomamanga imeanza kutoa maua. Huko ndiko nitakapokupatia pendo langu. Harufu nzuri ya tunguja imejaa hewani karibu na milango yetu kuna kila aina ya matunda bora, yote mapya na ya siku za nyuma, ambayo nimekuwekea wewe mpenzi wangu. Laiti ungekuwa kaka yangu, ambaye amenyonyeshwa na mama yangu! Hivyo, hata kama ningekutana nawe nje, ningekubusu na hakuna ambaye angenidharau. Ningekuongoza na kukufikisha nyumbani kwa mama mzazi, mahali ambapo ungenifundisha upendo. Ningekupa divai nzuri iliyokolezwa, ningekupa divai yangu ya makomamanga yangu. Mkono wako wa kushoto u chini ya kichwa changu, na mkono wako wa kulia wanikumbatia. Nawasihini, enyi wanawake wa Yerusalemu, msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi, hadi hapo wakati wake utakapofika. Ni nani huyu ajaye kutoka mbugani, huku anamwegemea mpenzi wake? Chini ya mtofaa, mimi nilikuamsha, pale ambapo mama yako aliona uchungu, naam, pale ambapo mama yako alikuzaa. Nipige kama mhuri moyoni mwako, naam, kama mhuri mikononi mwako. Maana pendo lina nguvu kama kifo, wivu nao ni mkatili kama kaburi. Mlipuko wake ni kama mlipuko wa moto, huwaka kama mwali wa moto. Maji mengi hayawezi kamwe kulizima, mafuriko hayawezi kulizamisha. Mtu akijaribu kununua pendo, akalitolea mali yake yote, atakachopata ni dharau tupu. Tunaye dada mdogo, ambaye bado hajaota matiti. Je, tumfanyie nini dada yetu siku atakapoposwa? Kama angalikuwa ukuta, tungalimjengea mnara wa fedha; na kama angalikuwa mlango, tungalimhifadhi kwa mbao za mierezi. Mimi nalikuwa ukuta, na matiti yangu kama minara yake. Machoni pake nalikuwa kama mwenye kuleta amani. Solomoni alikuwa ana shamba la mizabibu, mahali paitwapo Baal-hamoni. Alilikodisha kwa walinzi; kila mmoja wao alilipa vipande elfu vya fedha. Shamba langu la mizabibu ni shamba langu mwenyewe, naam, ni shamba langu binafsi! Basi, Solomoni, wewe ukae na elfu zako za fedha, na kila mlinzi wa matunda akae na mia mbili zake. Ewe uliye shambani, rafiki zangu wanasikiliza sauti yako; hebu nami niisikie tafadhali! Njoo haraka ewe mpenzi wangu, kama paa au mwanapaa dume juu ya milima ya manukato. Maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi, kuhusu Yuda na mji wa Yerusalemu, nyakati za utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Sikilizeni enyi mbingu, tega sikio ee dunia. Mimi nimewalea wanangu wakakua, lakini sasa wameniasi! Ngombe humfahamu mwenyewe, punda hujua kibanda cha bwana wake; lakini Waisraeli hawajui, watu wangu, hawaelewi!” Ole wako wewe taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, wazawa wa wenye kutenda maovu, watu waishio kwa udanganyifu! Nyinyi mmemwacha Mwenyezi-Mungu, mmemdharau Mtakatifu wa Israeli, mmefarakana naye na kurudi nyuma. Kwa nini huachi uasi wako? Mbona wataka kuadhibiwa bado? Kichwa chote ni majeraha matupu, na moyo wote unaugua! Toka wayo hadi kichwa hamna penye nafuu, umejaa majeraha na vidonda vitoavyo damu, navyo havikuoshwa, kufungwa wala kutiwa mafuta. Nchi yenu imeharibiwa kabisa; miji yenu imeteketezwa kwa moto. Wageni wananyakua nchi yenu mkiona kwa macho, imeharibiwa kama uharibifu wa Sodoma. Mji Siyoni umeachwa kama kibanda shambani, kama kitalu katika shamba la matango, kama mji uliozingirwa. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asingalituachia wachache, tungalikwisha kuwa kama watu wa Sodoma, tungalikuwa hali ileile ya Gomora. Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu enyi watawala waovu kama wa Sodoma! Sikilizeni mafunzo ya Mungu wetu enyi watu waovu kama wa Gomora! Mwenyezi-Mungu asema hivi; “Wingi wa tambiko zenu ni kitu gani kwangu? Nimezichoka sadaka zenu za kondoo wa kuteketezwa na mafuta ya wanyama wenu wanono. Sipendezwi na damu ya fahali, wala ya wanakondoo, wala ya beberu. Mnapokuja mbele yangu kuniabudu nani aliyewataka mkanyagekanyage nyua zangu? Msiniletee tena matoleo yenu yasiyo na maana; ubani ni chukizo kwangu. Acheni kufanya sikukuu za mwezi mpya, Sabato na mikutano mikubwa ya ibada; sikubali ibada zilizochanganyika na dhambi. Sikukuu zenu za mwezi mpya na nyinginezo moyo wangu wazichukia. Zimekuwa mzigo mzito kwangu, nami nimechoka kuzivumilia. “Mnapoinua mikono yenu kuomba nitauficha uso wangu nisiwaone. Hata mkiomba kwa wingi sitawasikia, maana mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu mbele yangu. Acheni kutenda maovu, jifunzeni kutenda mema. Tendeni haki, ondoeni udhalimu, walindeni yatima, teteeni haki za wajane.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Njoni, basi, tuhojiane. Ingawa mna madoa mekundu ya dhambi, mtatakaswa na kuwa weupe kama theluji; madoa yenu yajapokuwa mekundu kama damu, mtakuwa weupe kama sufu. Mkiwa tayari kunitii, mtakula mazao mema ya nchi. Lakini mkikaidi na kuniasi, mtaangamizwa kwa upanga. Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema.” Jinsi gani mji uliokuwa mwaminifu sasa umegeuka kuwa kahaba! Wakati mmoja haki ilitawala humo, lakini sasa umejaa wauaji. Fedha yenu imekuwa takataka; divai yenu imechanganyika na maji. Viongozi wako ni waasi; wanashirikiana na wezi. Kila mmoja anapenda hongo, na kukimbilia zawadi. Hawawatetei yatima, haki za wajane si kitu kwao. Kwa hiyo asema Bwana Mwenyezi-Mungu, Mwenye Nguvu wa Israeli: “Nitawamwagia maadui zangu hasira yangu, nitawalipiza kisasi wapinzani wangu. Nitanyosha mkono wangu dhidi yenu; nitayeyusha uchafu wenu kabisa, na kuondoa takataka yenu yote. Nitawapeni waamuzi wenu kama kwanza na washauri wenu kama pale awali. Ndipo Yerusalemu utakapoitwa ‘Mji wa Uadilifu’ utaitwa ‘Mji Mwaminifu’” Mji Siyoni utakombolewa kwa haki, uadilifu utawaokoa watakaotubu humo. Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa pamoja; wanaomwacha Mwenyezi-Mungu watateketezwa. Mtaionea aibu hiyo mialoni mliyoipenda sana; mtafadhaika kwa sababu ya bustani mlizofurahia. Mtakuwa kama mwaloni unaonyauka majani; kama shamba lisilo na maji. Wenye nguvu watakuwa kama majani makavu, matendo yao yatakuwa kama cheche za moto. Watateketea pamoja na matendo yao, wala hapatakuwa na mtu wa kuwaokoa. Neno alilopewa Isaya, mwana wa Amozi, kuhusu Yuda na Yerusalemu. Siku zijazo mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu utaimarishwa kupita milima yote, utainuliwa juu ya vilima vyote. Mataifa yote yatamiminika huko, watu wengi wataujia na kusema, “Njoni tupande mlima wa Mwenyezi-Mungu, twende nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, apate kutufundisha njia zake, nasi tuishi kadiri ya mwongozo wake. Maana sheria itakuja kutoka Siyoni; neno la Mwenyezi-Mungu kutoka Yerusalemu.” Mungu atasuluhisha mizozo ya mataifa atakata mashauri ya watu wengi. Watu watafua panga za vita kuwa majembe na mikuki yao kuwa miundu ya kupogolea. Taifa halitapigana na taifa lingine wala hayatafanya tena mazoezi ya vita. Sasa, enyi wazawa wa Yakobo, njoni, tutembee katika mwanga wa Mwenyezi-Mungu. Sasa, ee Mungu, umewatupa watu wako, wazawa wa Yakobo. Maana kweli wachawi wa mashariki wamejaa kati yao, wapo na wapiga ramli kama kwa Wafilisti. Wanashirikiana na watu wageni. Nchi yao imejaa fedha na dhahabu, hazina yao ni kubwa kupindukia. Nchi yao imejaa farasi, magari yao ya kukokotwa hayana idadi. Nchi yao imejaa vinyago vya miungu, huabudu kazi ya mikono yao, vitu walivyotengeneza wao wenyewe. Kwa hiyo, kila mtu ataaibishwa na kufedheheshwa. Usiwasamehe hata kidogo, ee Mungu! Ingieni katika mwamba, mkajifiche mavumbini, kuiepa hasira ya Mwenyezi-Mungu, mbali na utukufu wa enzi yake. Siku yaja ambapo kiburi cha watu kitashushwa, majivuno ya kila mtu yatavunjwa; na Mwenyezi-Mungu peke yake atatukuzwa siku hiyo. Naam, yaja siku ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi dhidi ya wenye kiburi na majivuno, dhidi ya wote wanaojikweza; dhidi ya mierezi yote ya Lebanoni, ambayo ni mirefu na mizuri, dhidi ya mialoni yote nchini Bashani; dhidi ya milima yote mirefu, dhidi ya vilima vyote vya juu; dhidi ya minara yote mirefu, dhidi ya kuta zote za ngome; dhidi ya meli zote za Tarshishi, na dhidi ya meli zote nzuri. Kiburi chote cha watu kitakomeshwa, majivuno ya kila mtu yatavunjwa. Na Mwenyezi-Mungu peke yake atatukuzwa siku hiyo. Vinyago vyote vya miungu vitatoweka kabisa. Ingieni katika mapango miambani, katika mashimo ardhini, kuiepa hasira ya Mwenyezi-Mungu, mbali na utukufu wa enzi yake, atakapokuja kuitia hofu dunia. Siku hiyo, watu watawatupia panya na popo vinyago vyao vya fedha na dhahabu walivyojitengenezea ili kuviabudu. Nao wataingia katika mapango miambani na kwenye nyufa za miamba, kuiepa hasira ya Mwenyezi-Mungu, mbali na utukufu wa enzi yake, atakapokuja kuitia hofu dunia. Usimwamini binadamu, uhai wake haudumu kama pumzi. Yeye anafaa kitu gani? Sasa, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi ataondoa kutoka Yerusalemu na Yuda kila tegemeo: Tegemeo lote la chakula, na tegemeo lote la kinywaji. Ataondoa mashujaa na askari, waamuzi na manabii, waaguzi na wazee, majemadari wa vikosi vya watu hamsini, na watu wenye vyeo, washauri, wachawi stadi na walozi hodari. Mungu ataweka watoto wawatawale; naam, watoto wachanga watawatawala. Watu watadhulumiana, kila mtu na jirani yake; vijana watawadharau wazee wao, na watu duni watapuuza wakuu wao. Wakati huo ndugu atamwambia ndugu yake wakiwa bado nyumbani kwa baba yao: “Wewe unalo koti; utakuwa kiongozi wetu. Chukua hatamu juu ya uharibifu huu!” Lakini siku hiyo atasema, “Mimi siwezi kuwa mwuguzi, nyumbani mwangu hamna chakula wala mavazi. Msinifanye mimi kuwa kiongozi wenu.” Watu wa Yerusalemu wamejikwaa, watu wa Yuda wameanguka, kwa kuwa wanampinga Mwenyezi-Mungu kwa maneno na matendo, wakipuuza utukufu wake miongoni mwao. Ubaguzi wao unashuhudia dhidi yao; wanatangaza dhambi yao kama ya Sodoma, wala hawaifichi. Ole wao watu hao, kwani wamejiletea maangamizi wenyewe. Waambieni waadilifu jinsi walivyo na bahati: Kwani watakula matunda ya matendo yao. Lakini ole wao watu waovu! Mambo yatawaendea vibaya, kwani waliyotenda yatawapata wao wenyewe. Watu wangu watadhulumiwa na watoto; wanawake ndio watakaowatawala. Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha, wanavuruga njia mnayopaswa kufuata. Mwenyezi-Mungu yu tayari kuanza mashtaka, anasimama kuwahukumu watu wake. Mwenyezi-Mungu anawashtaki wazee na wakuu wa watu wake: “Nyinyi ndio mlioliharibu shamba la mizabibu; mali walizowanyanganywa maskini zimo nyumbani kwenu. Mnamaanisha nini kuwakandamiza watu wangu, kuwatendea ukatili watu maskini? Nauliza mimi Bwana, Mwenyezi-Mungu wa majeshi.” Mwenyezi-Mungu asema: “Wanawake wa Siyoni wana kiburi; wanatembea wameinua shingo juu, wakipepesa macho yao kwa tamaa. Hatua zao ni za maringo, na miguuni njuga zinalia. Basi, mimi Mwenyezi-Mungu nitawaadhibu; nitawanyoa nywele hao wanawake wa Siyoni, na kuwavua nguo za kufunika uchi wao.” Siku yaja ambapo Mwenyezi-Mungu atawanyanganya wanawake wa Yerusalemu vitu vyote wanavyoringia: Njuga, kaya, mikufu, vipuli, vikuku, shungi, vitambaa vya kichwani, bangili, vibwebwe, vibweta vya marashi, hirizi, pete, hazama, mavazi ya sikukuu, mitandio, majoho, mikoba, mavazi yaoneshayo, mavazi ya kitani, vilemba na shela. Badala ya kunukia marashi watatoa uvundo; badala ya mishipi mizuri watatumia kamba; badala ya nywele nzuri watakuwa na upara; badala ya mavazi mazuri watavaa matambara; uzuri wao wote utageuka kuwa aibu. Wanaume wenu wataangamia kwa upanga, watu wenu wenye nguvu watakufa vitani. Malango ya mji yatalia na kuomboleza; nao mji utakuwa kama mwanamke aliyepokonywa kila kitu, ameketi mavumbini. Wakati huo wanawake saba watamvamia mwanamume mmoja na kumwambia, “Chakula na mavazi tutajitafutia wenyewe, lakini wewe utuondolee aibu yetu, uturuhusu tuitwe kwa jina lako.” Siku ile, tawi atakalochipusha Mwenyezi-Mungu litakuwa zuri na tukufu, nayo matunda ya nchi yatakuwa ya fahari na utukufu kwa wale Waisraeli watakaosalia. Waisraeli watakaobaki watayaonea fahari na kujivunia mazao ya nchi yao. Wale watakaosalia hai mjini Yerusalemu, naam, wale watakaobaki huko Siyoni, wataitwa “Wateule wa Mungu;” hao ndio wale wote watakaokuwa wameandikwa kitabuni mwake waishi huko Yerusalemu. Kwa roho yake, Bwana atawaweka sawa na kuwatakasa. Na atakapokwisha kuwatakasa wanawake wa Siyoni uchafu wao na kufuta madoa ya damu yaliyomo humo Yerusalemu, hapo atafanya kila mahali juu ya mlima Siyoni na juu ya mikutano ya watu kuwe na wingu wakati wa mchana, na moshi na moto uwakao vizuri wakati wa usiku. Zaidi ya hayo utukufu wa Mungu utaufunika na kuulinda mji wote. Utukufu wake utakuwa kwao kivuli kuwakinga na joto la mchana; na kimbilio na kinga yao wakati wa dhoruba na mvua. Nitaimba juu ya rafiki yangu, wimbo wa rafiki yangu na shamba lake la mizabibu: Rafiki yangu alikuwa na shamba la mizabibu juu ya kilima chenye rutuba nyingi. Alililima vizuri na kuondoa mawe yote, akaotesha humo mizabibu iliyochaguliwa; alijenga mnara wa ulinzi katikati yake, akachimba kisima cha kusindikia divai. Kisha akangojea lizae zabibu, lakini likazaa zabibu chungu. Kwa hiyo rafiki yangu anasema hivi: “Enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda, amueni tafadhali kati yangu na shamba langu. Ni kitu gani nilichokosa kulifanyia shamba langu? Na nilipotazamia lizae zabibu nzuri, mbona basi, likazaa zabibu chungu? “Na sasa nitawaambieni nitakavyolifanya hilo shamba langu. Nitauondoa ua wake, nalo litaharibiwa. Nitaubomoa ukuta wake, nalo litakanyagwakanyagwa. Nitaliacha liharibiwe kabisa, mizabibu yake haitapogolewa wala kupaliliwa. Litaota mbigili na miiba. Tena nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.” Naam! Shamba la mizabibu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi ni jumuiya ya Waisraeli, na mizabibu mizuri aliyoipanda ni watu wa Yuda. Yeye alitazamia watende haki, badala yake wakafanya mauaji; alitazamia uadilifu, badala yake wakasababisha kilio! Ole wao wanaonunua nyumba baada ya nyumba, wanaoongeza mashamba juu ya mashamba yao, mpaka kila sehemu inakuwa mali yao, na hamna nafasi kwa wengine nchini. Nimemsikia Mwenyezi-Mungu wa majeshi akitamka hivi: “Hakika nyumba nyingi zitabaki tupu, majumba makubwa mazuri bila wakazi. Shamba la mizabibu la eka kumi litatoa lita nane tu za divai; anayepanda kilo 100 za mbegu atavuna kilo 10 tu za nafaka.” Ole wao wanaoamka asubuhi na mapema wapate kukimbilia kunywa kileo; wanaokesha hata usiku, mpaka divai iwaleweshe! Katika karamu zao, hapakosekani vinubi, zeze, matari, filimbi na divai. Lakini hawajali matendo ya Mwenyezi-Mungu, wala kuzitambua kazi za mikono yake. Kwa hiyo, watu wangu watapelekwa uhamishoni kwa sababu ya utovu wao wa akili. Watu wenu mashuhuri watakufa njaa, watu wengi watakufa kwa kiu. Kuzimu inawangoja kwa hamu kubwa, imepanua kinywa chake mpaka mwisho. Waheshimiwa pamoja na raia wa Yerusalemu wanaingia humo makundi kwa makundi, kadhalika na wote wanaousherehekea. Kila mtu atafedheheshwa, na wenye kiburi wote wataaibishwa. Lakini Mwenyezi-Mungu wa majeshi atatukuzwa. Yeye huonesha ukuu wake kwa matendo yake ya haki, kwa kuwahukumu watu wake. Wanakondoo, wanambuzi na ndama, watapata malisho yao kwenye magofu ya miji yao, kana kwamba hizo ni sehemu za malisho yao. Ole wao wanaoburuta uovu kama kwa kamba; wanaokokota dhambi kama kwa kamba za mkokoteni. Wanasema: “Mwache Mwenyezi-Mungu afanye haraka, tunataka kuyaona aliyosema atayafanya! Mtakatifu wa Israeli na atimize kusudi lake. Hebu na tuone ana mipango gani!” Ole wao wanaosema uovu ni wema na wema ni uovu. Giza wanasema ni mwanga na mwanga wanasema ni giza. Kichungu wanasema ni kitamu na kitamu wanakiona kuwa kichungu. Ole wao wanaojiona kuwa wenye hekima ambao wanajiona kuwa wenye akili. Ole wao mabingwa wa kunywa divai, hodari sana wa kuchanganya vileo. Kwa hongo kidogo wanawaachilia wenye hatia na kuwanyima wasio na hatia haki yao. Kwa hiyo, kama moto uteketezavyo nyasi, kama majani yateketeavyo katika mwali wa moto ndivyo na mizizi yao itakavyooza, na maua yao yatakavyopeperushwa juu kama vumbi. Maana wameiacha sheria ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi, wamedharau neno la yule Mtakatifu wa Israeli. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwawakia watu wake, akaunyosha mkono wake dhidi yao, akawachapa, hata milima ikatetemeka, maiti zao zikawa kama takataka katika barabara za mji. Hata hivyo, hasira yake haikutulia, mkono wake bado ameunyosha kuwaadhibu. Mwenyezi-Mungu analiashiria taifa la mbali; anawapigia mruzi watu kutoka miisho ya dunia; nao waja mbio na kuwasili haraka! Hawachoki wala hawajikwai; hawasinzii wala hawalali; hakuna mshipi wao uliolegea wala kamba ya kiatu iliyokatika. Mishale yao ni mikali sana, pinde zao zimevutwa tayari. Kwato za farasi wao ni ngumu kama mawe; mwendo wa magurudumu ya magari ni kimbunga. Askari wao wananguruma kama simba; wananguruma kama wanasimba ambao wamekamata mawindo yao na kuwapeleka mahali mbali ambapo hakuna awezaye kuwanyanganya. Siku hiyo, watanguruma juu ya Israeli kama mvumo wa bahari iliyochafuka. Atakayeiangalia nchi kavu ataona giza tupu na dhiki, mwanga utafunikwa na mawingu. Mnamo mwaka aliofariki mfalme Uzia, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi kilicho juu na cha fahari. Pindo la vazi lake lilienea hekaluni mote, na juu yake walikuwa wamekaa malaika. Kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Mawili ya kufunika uso, mawili ya kufunika mwili na mawili ya kurukia. Waliitana kila mmoja na mwenzake hivi: “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu, ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi! Dunia yote imejaa utukufu wake.” Sauti yao iliitikisa misingi ya milango ya hekalu, nalo likajaa moshi. Basi, mimi nikasema, “Ole wangu! Mimi nimeangamia, maana, midomo yangu ni najisi, na watu ninaoishi nao ni najisi kama mimi. Hata hivyo, kwa macho yangu mwenyewe, nimemwona Mfalme, Mwenyezi-Mungu wa majeshi.” Basi, mmoja wa hao malaika akaruka kunijia, akiwa ameshika mkononi koleo lililokuwa na kaa la moto alilolitwaa madhabahuni. Naye akinigusa nalo mdomoni, akasema: “Tazama, kaa hili limekugusa mdomo; umeondolewa hatia yako, umesamehewa dhambi yako.” Kisha nikamsikia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekuwa mjumbe wetu?” Nami nikajibu, “Niko hapa! Nitume mimi.” Naye akaniambia, “Nenda ukawaambie watu hawa: ‘Mtasikiliza sana, lakini hamtaelewa; mtatazama sana, lakini hamtaona.’” Kisha akaniambia, “Zipumbaze akili za watu hawa, masikio yao yasisikie, macho yao yasione; ili wasije wakaona kwa macho yao, wakasikia kwa masikio yao, wakaelewa kwa akili zao, na kunigeukia, nao wakaponywa.” Mimi nikauliza, “Bwana, mpaka lini?” Naye akanijibu, “Mpaka hapo miji itakapobaki tupu bila wakazi, nyumba bila watu, na nchi itakapoharibiwa kabisa. Nami Mwenyezi-Mungu nitawapeleka watu mbali, na kuifanya nchi yote kuwa mahame. Hata wakibaki watu asilimia kumi, nao pia watateketezwa. Hao watakuwa kama mvinje au mwaloni ambao kisiki chake kimebaki baada ya kukatwa.” (Kisiki hicho ni mbegu takatifu ya chanzo kipya.) Wakati mfalme Ahazi mwana wa Yothamu na mjukuu wa Uzia, alipokuwa anatawala Yuda, Resini, mfalme wa Aramu, na Peka mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, waliushambulia mji wa Yerusalemu, lakini hawakuweza kuuteka. Mfalme wa Yuda alipopata habari kwamba Waashuru wanashirikiana na Waisraeli, yeye pamoja na watu wote wa Yuda waliogopa na kutetemeka kama miti inayotikiswa na upepo. Mwenyezi-Mungu akamwambia Isaya, “Mchukue mwanao, Shearyashubu, uende kukutana na mfalme Ahazi. Utamkuta barabarani mahali wanapofanyia kazi watengenezaji nguo, mwisho wa mfereji uletao maji kutoka bwawa la juu. Mwambie awe macho, atulie na asiogope wala asife moyo, kwa sababu ya hasira kali ya mfalme Resini wa Ashuru, na ya mwana wa Remalia. Hao wawili ni kama tu moshi wa kuni zinazozimika. Waashuru, kadhalika na Peka pamoja na jeshi la Efraimu wamefanya mpango mbaya dhidi yako. Wamesema, ‘Twende kuivamia nchi ya Yuda, tuwatie watu hofu, tuitwae nchi na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme wao.’ “Lakini mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Jambo hilo halitafaulu kamwe. Kwani mji mkuu wa Aramu ni Damasko, na huyo Resini ni mkuu wa Damasko tu. Mji mkuu wa Efraimu ni Samaria, na mwana wa Remalia ni mkuu wa Samaria tu. Mnamo miaka sitini na mitano utawala wa Efraimu utavunjwa; Efraimu halitakuwa taifa tena. Kama hutaamini hutaimarika.” *** Tena Mwenyezi-Mungu akamwambia Ahazi, “Mwombe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, akupe ishara; iwe ni kutoka chini kuzimu au juu mbinguni.” Ahazi akajibu, “Sitaomba ishara! Sitaki kumjaribu Mwenyezi-Mungu.” Basi, Isaya akamjibu, “Sikiliza basi, enyi watu wa ukoo wa Daudi! Je, haitoshi kuwachosha watu hata sasa mnataka kumchosha Mungu wangu pia? Haya basi, Bwana mwenyewe atawapa ishara: Msichana atachukua mimba, atajifungua mtoto wa kiume na kumwita jina lake Emanueli. Atakula siagi na asali mpaka atakapojua kukataa mabaya na kuchagua mema. Maana, kabla mtoto huyo hajajua kukataa maovu na kuchagua mema, nchi za wafalme hao wawili unaowaogopa zitakuwa mahame. Mwenyezi-Mungu atakuletea wewe pamoja na watu wako na jamii yote ya kifalme siku za taabu kuliko zile zote zilizowahi kutokea tangu wakati watu wa Efraimu walipojitenga na Yuda; yaani, atawaleteeni mfalme wa Ashuru.” Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atawapigia mruzi watu wa Misri waje kama nzi toka vijito vya mto Nili; na watu wa Ashuru waje kama nyuki kutoka nchi yao. Watakuja makundi kwa makundi na kuyajaza mabonde yaliyopasukapasuka, mapango miambani, miiba, vichaka vyote na malisho yote. Wakati huo, Bwana atakopa wembe kutoka ngambo ya mto Eufrate, yaani mfalme wa Ashuru. Atawanyoa vichwa vyenu, miili yenu na kukatilia mbali pia ndevu zenu. Wakati huo, mtu atafuga ng'ombe mmoja mchanga na kondoo wawili; nao watatoa maziwa kwa wingi hata aweze kula siagi. Watu watakaosalia katika nchi watakula siagi na asali. Wakati huo, kila mahali palipokuwa na mashamba ya mizabibu kwa maelfu ya thamani ya fedha 1,000 kwa kipimo cha hekalu yatakuwa mbigili na miiba mitupu. Watu watakwenda huko kuwinda kwa pinde na mishale, maana nchi yote itakuwa imejaa mbigili na miiba. Nayo milima yote iliyokuwa ikilimwa itakuwa imejaa mbigili na miiba, hata hakuna mtu atakayejaribu kwenda huko, badala yake itakuwa malisho ya ng'ombe na kondoo. Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Chukua ubao mkubwa, uandike juu yake maneno yanayosomeka kwa urahisi: ‘TEKA-HARAKA-POKONYA-UPESI.’” Basi, nikajipatia mashahidi wawili waaminifu ambao wangenishuhudia: Kuhani Uria na Zekaria, mwana wa Yeberekia. Nililala na mke wangu ambaye pia ni nabii, akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Mpe mtoto huyo jina ‘Teka-haraka-pokonya-upesi.’ Maana kabla mtoto huyu hajafikia umri wa kuweza kutamka: ‘Baba’ au ‘Mama,’ utajiri wa Damasko na nyara walizoteka huko Samaria zitapelekwa kwa mfalme wa Ashuru.” Mwenyezi-Mungu aliongea nami tena, akaniambia, “Kwa kuwa watu hawa wameyakataa maji ya Shiloa yatiririkayo polepole, wakafa moyo mbele ya mfalme Resini na mfalme Peka mwana wa Remalia, basi, mimi Bwana nitawaletea mafuriko makuu ya maji ya mto Eufrate yaani mfalme wa Ashuru na nguvu zake zote; yatafurika na kupita kingo zake. Utaingia nchini Yuda kwa nguvu na kufurika na kupanda mpaka shingoni; utaenea juu ya nchi yako yote, ee Emanueli!” Unganeni enyi watu wa mataifa nanyi mtafedheheshwa! Sikilizeni enyi nchi za mbali duniani! Jiwekeni tayari na kufedheheshwa; naam, kaeni tayari na kufedheheshwa. Shaurianeni pamoja lakini itakuwa bure; fanyeni mipango lakini haitafaulu, maana Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi-Mungu alinionya kwa nguvu nisifuate njia za watu hawa, akaniambia, “Usijumuike nao katika njama zao, wala usiogope yale wanayoyaogopa wala kuwa na hofu. Nitambue mimi peke yangu, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kuwa mtakatifu; utaniogopa na kunicha mimi peke yangu. Mimi nitakuwa kimbilio, nitakuwa pia kama jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuziangusha falme za Israeli na Yuda; nitakuwa mtego wa kuwatega na kuwanasa wakazi wa Yerusalemu. Watu wengi watajikwaa, wataanguka na kupondeka; watanaswa katika mtego huo na kuchukuliwa mateka.” Nitalihifadhi agizo hilo na kulifunga fundisho hilo miongoni mwa wafuasi wangu. Nitamngojea Mwenyezi-Mungu ambaye amejificha mbali na wazawa wa Yakobo; nitamtumainia. Mimi pamoja na watoto alionipa Mwenyezi-Mungu ni ishara na alama katika Israeli kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi akaaye mlimani Siyoni. Baadhi watawaambieni: “Nendeni mkatake shauri kwa mizimu na mizuka iliayo kama ndege; kwani ni kawaida watu kutaka shauri kwa miungu yao, na kutaka shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai.” Hakika anayesema hivyo hajapata kuona mwanga. Lakini nyinyi shikilieni lile agizo na fundisho la Mungu. Watu watatangatanga nchini wamefadhaika sana na wenye njaa. Na wakiwa na njaa, hasira zitawawaka na kumlaani mfalme wao kadhalika na Mungu wao. Watatazama juu mbinguni na kuiangalia dunia, lakini wataona tu taabu, giza na mauzauza ya shida. Hakuna atakayeliepa giza hilo kuu. Lakini nchi ile iliyokuwa imekumbwa na huzuni haitabaki daima katika giza hilo kuu. Hapo awali Mungu alizifedhehesha nchi za Zebuluni na Naftali, lakini siku za usoni ataifanikisha sehemu hii ya baharini na nchi iliyo ngambo ya Yordani na hata Galilaya wanamoishi watu wa mataifa. Watu waliotembea gizani wameona mwanga mkubwa. Watu walioishi katika nchi ya giza kuu, sasa mwanga umewaangazia. Wewe, ee Mungu, umelikuza taifa, umeiongeza furaha yake. Watu wanafurahi mbele yako, wana furaha kama wakati wa mavuno, kama wafurahivyo wanaogawana nyara. Maana nira nzito walizobeba, nira walizokuwa wamefungwa, na fimbo ya wanyapara wao, umezivunjavunja kama wakati wa Wamidiani. Viatu vyote vya washambulizi vitani na mavazi yote yenye madoa ya damu yatateketezwa kama kuni za kuwasha moto. Maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto wa kiume. Naye atapewa mamlaka ya kutawala. Ataitwa: “Mshauri wa Ajabu”. “Mungu Mwenye Nguvu”, “Baba wa Milele”, “Mfalme wa Amani”. Utawala wake utastawi daima, amani ya ufalme wake haitakoma. Atachukua wadhifa wa mfalme Daudi na kutawala juu ya ufalme wake; ataustawisha na kuuimarisha, kwa haki na uadilifu, tangu sasa na hata milele. Hayo atayafanya Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mwenyezi-Mungu ametoa tamko dhidi ya Yakobo nalo litampata Israeli. Watu wote watatambua, ukoo wote wa Efraimu na wakazi wa Samaria. Kwa kiburi na majivuno wanasema: “Kuta za matofali zimeanguka lakini sisi tutazijenga kwa mawe yaliyochongwa! Nyumba za boriti za mikuyu zimeharibiwa lakini mahali pake tutajenga za mierezi.” Basi, Mwenyezi-Mungu atawaletea wapinzani na kuwachochea maadui zao. Waaramu upande wa mashariki, Wafilisti upande wa magharibi, wamepanua vinywa vyao kuimeza Israeli. Hata hivyo, hasira yake haijatulia, bado ameunyosha mkono wake. Ingawa aliwaadhibu watu, hawakumrudia Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Basi kwa muda wa siku moja tu, Mwenyezi-Mungu atakata katika Israeli vichwa na mikia, tawi la mtende na nyasi: Vichwa ndio wazee na waheshimiwa, mikia ndio manabii wafundishao uongo. Wale wanaoongoza watu hawa wamewapotosha, na hao wanaoongozwa nao wamepotoka. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu hawahurumii vijana wao, hana huruma juu ya yatima na wajane wao; kwani hakuna hata mmoja amchaye Mungu, kila mtu husema uongo. Hata hivyo, hasira yake haijatulia, bado ameunyosha mkono wake. Uovu huwaka kama moto uteketezao mbigili na miiba; huwaka kama moto msituni, na kutoa moshi mzito upandao angani juu. Kwa ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi nchi imechomwa moto, na watu ni kama kuni za kuuwasha. Hakuna mtu anayemhurumia ndugu yake; wananyanganya upande mmoja na hawatosheki; wanakula upande mwingine lakini hawashibi. Kila mmoja anamshambulia mwenzake. Manase dhidi ya Efraimu, Efraimu dhidi ya Manase na wote wawili dhidi ya Yuda. Hata hivyo, hasira ya Mwenyezi-Mungu haijatulia, bado ameunyosha mkono wake. Ole wao wanaotunga sheria zisizo za haki, watu wanaopitisha sheria za kukandamiza. Huwanyima maskini haki zao, na kuwaibia maskini wa watu wangu maslahi yao. Wajane wamekuwa nyara kwao; yatima wamekuwa mawindo yao. Je, mtafanya nini siku ya adhabu, siku dhoruba itakapowajieni kutoka mbali? Mtamkimbilia nani kuomba msaada? Mtakwenda wapi kuweka mali yenu? Litakalowabakia ni kujikunyata kati ya wafungwa na kuangamia pamoja na wanaouawa vitani. Hata hivyo, hasira ya Mwenyezi-Mungu haijatulia, bado ameunyosha mkono wake. Ole wake Ashuru, fimbo ya hasira yangu, yeye ashikaye kiboko cha hasira yangu! Nilimtuma kuliadhibu taifa ovu, nilimwamuru kuwaadhibu watu niliowakasirikia, kuwapora na kuteka nyara, na kuwakanyaga chini kama tope njiani. Lakini Ashuru hakudhamiria hivyo, yeye alikuwa na nia nyingine; alikusudia kuharibu kabisa, kuangamiza mataifa mengi iwezekanavyo. Maana alisema: “Je, si kweli majemadari wangu ni wafalme? Je, si kweli kwamba Kalno nitautenda kama Karkemishi, mji wa Hamathi kama mji wa Arpadi, Samaria kama Damasko? Kama nimefaulu kuunyosha mkono wangu dhidi ya falme zenye sanamu za miungu kubwa kuliko sanamu za Yerusalemu na Samaria; je, nitashindwa kuutenda Yerusalemu na sanamu zake, kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake?” Wakati Mwenyezi-Mungu atakapomaliza kazi zake zote mlimani Siyoni na mjini Yerusalemu, atamwadhibu mfalme wa Ashuru, kwa sababu ya majivuno na kiburi chake. Maana mfalme wa Ashuru alisema: “Kwa nguvu zangu mwenyewe nimetenda hayo, na kwa hekima yangu, maana mimi ni mwerevu! Nimeondoa mipaka kati ya mataifa, nikazipora hazina zao; kama fahali nimewaporomosha walioketia viti vya enzi. Kama mtu anyoshaye mkono kwenye kiota, ndivyo nilivyochukua mali yao; kama mtu aokotavyo mayai yaliyoachwa kiotani, ndivyo nilivyowaokota duniani kote, wala hakuna mtu aliyeweza kupiga bawa, au aliyefungua kinywa kunipigia kelele.” Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Je, shoka litajigamba dhidi ya anayelitumia? Msumeno waweza kujivuna dhidi ya mwenye kukata nao? Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua anayeishika, au mkongojo kumwinua mwenye kuutumia!” Kwa hiyo, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, atawaletea askari wao ugonjwa wa kuwakondesha, na fahari yao itateketezwa kama kwa moto. Mungu aliye mwanga wa Israeli atakuwa kama moto, Mtakatifu wa Israeli atakuwa mwali wa moto ambao kwa siku moja utateketeza kila kitu: Miiba yake na mbigili zake pamoja. Misitu yake ya fahari na mashamba yake mazuri, Mwenyezi-Mungu atayaangamiza yote; itakuwa kama mtu aliyemalizwa na ugonjwa. Miti itakayobaki msituni mwake itakuwa michache sana hata mtoto mdogo ataweza kuihesabu. Siku ile wazawa wa Yakobo watakaobaki, naam, Waisraeli watakaosalia hawatalitegemea tena taifa lililowaadhibu, bali watamtegemea kabisa Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli. Wazawa wa Yakobo wachache watakaobaki watamrudia Mungu Mkuu. Maana, hata kama sasa Waisraeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaorudi. Maangamizi yamepangwa yafanyike, nayo yatafanyika kwa haki tupu. Naam! Bwana, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, atakamilisha kabisa katika nchi yote jambo aliloamua kutenda. Kwa hiyo, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Enyi watu wangu mnaokaa Siyoni msiwaogope Waashuru ambao wanawapiga kwa fimbo, wakiinua mikongojo yao dhidi yenu kama walivyofanya Wamisri. Maana bado kitambo, nayo hasira yangu itapita na ghadhabu yangu itawageukia Waashuru. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi na nitawachapa kama nilivyowachapa Wamidiani kwenye jabali la Orebu. Nitanyosha fimbo yangu juu ya bahari kuwachapa kama nilivyowafanya Wamisri. Wakati huo, mzigo waliowabebesha nitauondoa na nira waliyowatia shingoni mwenu itavunjwa.” Adui amepanda kutoka Rimoni, amefika mjini Ayathi. Amepitia huko Migroni, mizigo yake ameiacha Mikmashi. Amekwisha pita kivukoni, usiku huu analala Geba. Watu wa Rama wanatetemeka kwa hofu, wakazi wa Gibea, mji wa Shauli, wamekimbia. Pazeni sauti enyi watu wa Galimu! Tegeni sikio enyi watu wa Laisha! Jibuni enyi wenyeji wa Anathothi! Watu wa Madmena wako mbioni, wakazi wa Gebimu wanakimbilia usalama. Leo hii, adui atatua Nobu, atatikisa ngumi yake dhidi ya mlima Siyoni; naam, atautikisia ngumi mji wa Yerusalemu. Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakata matawi yake kwa ukatili; miti mirefu itaangushwa chini, walio juu wataaibishwa. Atakata vichaka vya msituni kwa shoka, Lebanoni na mierezi yake maarufu itaanguka. Kutatokea chipukizi katika kisiki cha Yese, tawi litachipua mizizini mwake. Roho ya Mwenyezi-Mungu itakaa kwake, roho ya hekima na maarifa, roho ya shauri jema na nguvu, roho ya ujuzi na ya kumcha Mwenyezi-Mungu. Atafurahia kumcha Mwenyezi-Mungu. Hatahukumu kadiri ya mambo ya njenje, wala kuamua kufuatana na yale anayosikia. Atawapatia haki watu maskini, atawaamulia sawasawa wanyonge nchini. Kwa neno lake ataiadhibu dunia, kwa tamko lake atawaua waovu. Haki itakuwa kama mkanda wa kujifunga, uaminifu utakaa naye kama mkanda kiunoni. Mbwamwitu ataishi pamoja na mwanakondoo, chui watapumzika pamoja na mwanambuzi. Ndama na wanasimba watakula pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ngombe na dubu watakula pamoja, ndama wao watapumzika pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe. Mtoto mchanga atacheza kwenye shimo la nyoka mtoto ataweza kutia mkono shimoni mwa nyoka wa sumu. Katika mlima mtakatifu wa Mungu hakutakuwa na madhara wala uharibifu. Maana kumjua Mwenyezi-Mungu kutaenea pote nchini, kama vile maji yajaavyo baharini. Siku ile chipukizi wa Yese atakuwa ishara kwa mataifa; mataifa yatamtafuta na makazi yake yatatukuka. Siku hiyo, Bwana ataunyosha mkono wake tena kuwarejesha watu wake waliosalia huko Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Shinari, Hamathi na sehemu za pwani. Naye atatweka bendera kuwaashiria mataifa, kuwakusanya Waisraeli waliodharauliwa, kuwaleta pamoja watu wa Yuda waliotawanywa, na kuwarudisha toka pembe nne za dunia. Wivu wa Efraimu juu ya Yuda utakoma, hakutakuwa tena na uadui kati ya Yuda na Efraimu. Wote pamoja watawavamia Wafilisti walio magharibi, pamoja watawapora watu wakaao mashariki. Watawashinda Waedomu na Wamoabu, nao Waamoni watawatii. Mwenyezi-Mungu atakausha ghuba ya bahari ya Shamu, kwa pumzi yake ichomayo atakausha mto Eufrate, nao utagawanyika katika vijito saba, watu wavuke humo miguu mikavu. Tena, kutakuwa na barabara kuu toka Ashuru kwa ajili ya watu wake waliobaki humo kama ilivyokuwa kwa Waisraeli wakati walipotoka nchini Misri. Siku hiyo mtasema: “Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, maana ingawa ulinikasirikia, hasira yako imetulia, nawe umenifariji. Mungu ndiye mwenye kuniokoa, nitamtegemea yeye, wala sitaogopa; Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu; yeye mwenyewe ndiye aniokoaye.” Mtachota maji kwa furaha kutoka visima vya wokovu. Siku hiyo mtasema: “Mshukuruni Mwenyezi-Mungu mwombeni kwa jina lake. Yajulisheni mataifa matendo yake, tangazeni kuwa jina lake limetukuka. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa kwa kuwa ametenda mambo makuu; haya na yajulikane duniani kote. Pazeni sauti na kuimba kwa furaha, enyi wakazi wa Siyoni, maana aliye mkuu miongoni mwenu ndiye Mungu, Mtakatifu wa Israeli.” Kauli ya Mungu dhidi ya Babuloni ambayo Isaya, mwana wa Amozi, alipewa katika maono: Mungu asema: “Twekeni bendera juu ya mlima usio na miti. Wapaazieni sauti askari wapungieni watu mkono waingie malango ya mji wa wakuu. Mimi nimewaamuru wateule wangu, nimewaita mashujaa wangu, hao wenye kunitukuza wakishangilia, waje kutekeleza lengo la hasira yangu.” Sikilizeni kelele milimani kama za kundi kubwa la watu! Sikilizeni kelele za falme, na mataifa yanayokusanyika! Mwenyezi-Mungu wa majeshi analikagua jeshi linalokwenda vitani. Wanakuja kutoka nchi za mbali, wanatoka hata miisho ya dunia: Mwenyezi-Mungu na silaha za hasira yake anakuja kuiangamiza dunia. Lieni maana siku ya Mwenyezi-Mungu imekaribia; inakuja kama maafa kutoka kwa Mungu Mwenye Nguvu. Kwa hiyo mikono ya kila mtu italegea, kila mtu atakufa moyo. Watu watafadhaika, watashikwa na hofu na maumivu, watakuwa na uchungu kama mama anayejifungua. Watatazamana kwa mashaka, nyuso zao zitawaiva kwa haya. Siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja, siku kali, ya ghadhabu na hasira kali. Itaifanya nchi kuwa uharibifu, itawaangamiza wenye dhambi wake. Nyota na vilimia vyake angani hazitaangaza; jua linapochomoza litakuwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nitauadhibu ulimwengu kwa uovu wake, waovu kwa sababu ya makosa yao. Nitakikomesha kiburi cha wenye majivuno, na kuporomosha ubaradhuli wa watu katili. Nitawafanya watu kuwa wachache kuliko dhahabu safi; binadamu watakuwa wachache kuliko dhahabu ya Ofiri. Nitazitetemesha mbingu nayo nchi itatikisika katika misingi yake kwa sababu ya ghadhabu yangu Mwenyezi-Mungu siku ile ya hasira yangu kali. “Kama swala anayewindwa, kama kondoo wasio na mchungaji, kila mmoja atajiunga na watu wake kila mtu atakimbilia nchini mwake. Yeyote atakayeonekana atatumbuliwa, atakayekamatwa atauawa kwa upanga. Watoto wao wachanga watapondwapondwa mbele yao, watanyanganywa nyumba zao, na wake zao watanajisiwa. “Ninawachochea Wamedi dhidi yao; watu ambao hawajali fedha wala hawavutiwi na dhahabu. Mishale yao itawaua vijana, hawatakuwa na huruma kwa watoto, wala kuwahurumia watoto wachanga. Babuloni johari ya falme zote na umaarufu wa kiburi cha Wakaldayo utakuwa kama Sodoma na Gomora, wakati Mungu alipoiangamiza. Kamwe hautakaliwa tena na watu, watu hawataishi humo katika vizazi vyote. Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake humo, wala mchungaji atakayechunga wanyama wake humo. Badala yake watakuwamo wanyama wakali wa porini, bundi watajaa katika nyumba zake. Mbuni wataishi humo, na majini yatachezea humo. Mbwamwitu watalia ndani ya ngome zake, mbweha wataonekana ndani ya nyumba zao za anasa. Wakati wa Babuloni umekaribia, wala siku zake hazitaongezwa.” Mwenyezi-Mungu atawahurumia tena watu wa Yakobo, atawateua tena Waisraeli. Atawarudisha katika nchi yao wenyewe, na wageni watakuja na kukaa pamoja na watu wa Yakobo. Watu wa mataifa watawasaidia Waisraeli kurudi katika nchi waliyopewa na Mwenyezi-Mungu. Na hapo watawatumikia Waisraeli kama watumwa. Wale waliowateka sasa watatekwa na Waisraeli, na watawatawala wale waliowadhulumu. Ewe Israeli, wakati Mwenyezi-Mungu atakapokufariji baada ya mateso, misukosuko na utumwa uliofanyiwa, utaimba utenzi huu wa kumdhihaki mfalme wa Babuloni: “Jinsi gani mdhalimu alivyokomeshwa! Ujeuri wake umekomeshwa! Mwenyezi-Mungu amelivunja gongo la waovu, ameivunja fimbo ya kifalme ya watawala, ambao walipiga nayo watu kwa hasira bila kukoma, na kuwatawala kwa udhalimu bila huruma. Sasa dunia yote ina utulivu na amani, kila mtu anaimba kwa furaha. Misonobari inafurahia kuanguka kwako, nayo mierezi ya Lebanoni pamoja yasema: ‘Kwa vile sasa umeangushwa, hakuna mkata miti atakayekuja dhidi yetu!’ “Kuzimu nako kumechangamka, ili kukulaki wakati utakapokuja. Kunaiamsha mizimu ije kukusalimu na wote waliokuwa wakuu wa dunia; huwaamsha kutoka viti vyao vya enzi wote waliokuwa wafalme wa mataifa. Wote kwa pamoja watakuambia: ‘Nawe pia umedhoofika kama sisi! Umekuwa kama sisi wenyewe! Fahari yako imeteremshwa kuzimu pamoja na muziki wa vinubi vyako. Chini mabuu ndio kitanda chako, na wadudu ndio blanketi lako!’ “Jinsi gani ulivyoporomoshwa toka mbinguni, wewe uliyekuwa nyota angavu ya alfajiri. Jinsi gani ulivyoangushwa chini, wewe uliyeyashinda mataifa! Wewe ulijisemea moyoni mwako: ‘Nitapanda mpaka mbinguni; nitaweka kiti changu juu ya nyota za Mungu, nitaketi juu ya mlima wakutanapo miungu, huko mbali pande za kaskazini. Nitapanda vilele vya mawingu nitajifanya kuwa sawa na Mungu Mkuu.’ Lakini umeporomoshwa hadi kuzimu; umeshushwa chini kabisa shimoni. “Watakaokuona watakukodolea macho, watakushangaa wakisema: ‘Je, huyu ndiye aliyetetemesha dunia na kuzitikisa falme, aliyegeuza dunia kuwa kama jangwa, akaangamiza miji yake, na kuwanyima wafungwa wake kurudi kwao?’ Wafalme wote wa mataifa wamezikwa kwa heshima kila mmoja ndani ya kaburi lake. Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako; kama mtoto wa kuchukiza aliyezaliwa mfu maiti yako imekanyagwakanyagwa, umerundikiwa maiti za waliouawa kwa upanga, waliotupwa mashimoni penye mawe. Lakini wewe hutaunganishwa nao katika mazishi, maana uliiharibu nchi yako, wewe uliwaua watu wako. Wazawa wa waovu na wasahaulike kabisa! Kaeni tayari kuwachinja watoto wake kwa sababu ya makosa ya baba zao, wasije wakaamka na kuimiliki nchi, na kuijaza dunia yote miji yao.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Nitaushambulia mji wa Babuloni na kuuangamiza kabisa. Nitaharibu kila kitu, mji wote, watoto na yeyote aliyebaki hai. Mimi Mwenyezi-Mungu nimenena. Nitaufanya kuwa makao ya nungunungu, na utakuwa madimbwi ya maji. Nami nitaufagilia mbali kwa ufagio wa maangamizi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimenena.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameapa: “Kama nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa; kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyokamilika. Nitauvunja uwezo wa Waashuru nchini mwangu; nitawakanyagakanyaga katika milima yangu. Nitawaondolea watu wangu nira ya dhuluma yao, na mzigo wa mateso yao.” Huu ndio uamuzi wake Mwenyezi-Mungu kuhusu dunia yote; hii ndiyo adhabu atakayotoa juu ya mataifa yote. Kama Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameamua, nani atakayeweza kubatilisha uamuzi wake? Kama amepania kutoa adhabu, ni nani atakayempinga? Mwaka alipofariki mfalme Ahazi, Mungu alitoa kauli hii: “Msishangilie enyi Wafilisti wote, kwamba Ashuru, fimbo iliyowapiga, imevunjika; maana, nyoka wa kawaida atazaa nyoka mwenye sumu, na nyoka mwenye sumu atazaa joka lirukalo. Wazaliwa wa kwanza wa maskini watashiba, na fukara watakaa kwa usalama. Lakini chipukizi wenu nitawaua kwa njaa; na yeyote wenu atakayebaki nitamuua. Piga yowe ewe lango; lia ewe mji; yeyuka kwa hofu ewe nchi yote ya Filistia. Maana moshi wa askari waja kutoka kaskazini, wala hakuna atakayechelewa katika majeshi yake.” Basi watapewa jibu gani wajumbe wa taifa hilo? Wataambiwa: Mwenyezi-Mungu ameijenga imara Siyoni, na maskini wa watu wake watakimbilia usalama huko. Kauli ya Mungu dhidi ya nchi ya Moabu. Mji wa Ari nchini Moabu umeangamizwa usiku; mji wa Kiri nchini Moabu umeteketezwa usiku. Watu wa Diboni wamepanda hekaluni, hadi mahali pa juu kuomboleza, watu wa Moabu wanalia kwa ajili ya Nebo na Medeba; vichwa vyote vimenyolewa upara, ndevu zao zote zimekatwa kabisa. Wanapita njiani wamevaa mavazi ya gunia. Kwenye paa za nyumba na viwanja vya mji watu wanalia na kukauka kwa machozi. Watu wa Heshboni na Eleale wanalia, sauti zao zinasikika hadi Yahazi. Hata askari wa Moabu wanalia kwa sauti; mioyo yao inatetemeka. Moyo wangu unasononeka juu ya nchi ya Moabu; wakimbizi wake wanakimbilia Soari, wanakimbia mpaka Eglath-shelishiya. Wanapanda njia ya kwenda Luhithi wakilia, njiani kwenda Horonaimu wanatoa kilio cha maangamizi. Kijito cha Nimrimu kimekauka; nyasi zimekauka, majani mabichi yamenyauka, hakuna chochote kinachoota hapo. Watu wanavuka kijito cha Mierebi wamebeba mali yao yote waliyochuma, na kila walichojiwekea kama akiba. Kilio kimezuka pote nchini Moabu, maombolezo yao yamefika Eglaimu, naam, yamefika mpaka Beer-elimu. Maji ya Diboni yamejaa damu, lakini Mungu ataongeza msiba wa Diboni. Hao wachache watakaobaki hai na kukimbia kutoka nchini Moabu, watapelekewa simba wa kuwaua. Pelekeni wanakondoo kwa mtawala wa nchi, pelekeni kutoka Sela jangwani mpaka mlimani Siyoni. Kama ndege wanavyohangaika na kurukaruka, wakiwa wamefukuzwa kutoka viota vyao, ndivyo walivyo mabinti wa Moabu kwenye vivuko vya Arnoni. Wamoabu wanawaambia watu wa Yuda, “Tupeni mwongozo, tuamulieni. Enezeni ulinzi wenu juu yetu, kama vile usiku uenezavyo kivuli chake. Tuficheni sisi wakimbizi; msitusaliti sisi tuliofukuzwa. Wakimbizi wa Moabu waishi kwenu, muwe kimbilio lao mbali na mwangamizi.” Mdhalimu atakapokuwa ametoweka, udhalimu utakapokuwa umekoma, na wavamizi kutoweka nchini, utawala adili utazinduliwa katika maskani ya Daudi, mtawala apendaye kutenda haki, na mwepesi wa kufanya yaliyo sawa; atatawala humo kwa uaminifu. Watu wa Yuda wanasema hivi: “Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu, tunajua jinsi alivyojivuna mno; tumesikia juu ya majivuno, kiburi na ufidhuli wake; lakini majivuno yake hayo ni bure.” Sasa Wamoabu wanalia; wote wanaomboleza juu ya nchi yao. Ombolezeni kwa pigo hilo kubwa, na juu ya maandazi ya zabibu za Kir-haresethi. Mashamba ya Heshboni yamefifia. Kadhalika na zabibu za Sibma ambazo ziliwalevya wakuu wa mataifa zikafika Yazeri na kusambaa hata jangwani, chipukizi zake zikafika hata ngambo ya bahari. Kwa hiyo ninalia pamoja na Yazeri kwa ajili ya mizabibu ya Sibma. Machozi yananitoka kwa ajili yenu, enyi miji ya Heshboni na Eleale; maana vigelegele vya mavuno ya matunda, vigelegele vya mavuno ya nafaka vimetoweka. Furaha na shangwe zimetoweka katika shamba la rutuba. Kwenye mizabibu hakuna kuimba tena, wala kupiga vigelegele. Hakuna tena kukamua zabibu shinikizoni, sauti za furaha za mavuno zimekomeshwa. Hivyo, nafsi yangu yalilia Moabu kama kinubi, na moyo wangu kwa ajili ya mji wa Kir-heresi. Watu wa Moabu wanapojitokeza kuabudu mungu wao, wanapojichosha huko juu mahali pa ibada, wanapokwenda mahali pao patakatifu kusali, hawatakubaliwa. Hili ndilo jambo alilosema Mwenyezi-Mungu wakati uliopita kuhusu Moabu. Lakini sasa Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Baada ya miaka mitatu kamili, ikihesabiwa kama mfanyakazi anavyohesabu siku zake, fahari ya Moabu itakwisha. Ingawa watu wake ni wengi, watakaobaki hai watakuwa wachache na wanyonge.” Kauli ya Mungu dhidi ya Damasko. “Damasko utakoma kuwa mji; utakuwa rundo la magofu. Mitaa yake imeachwa mahame milele. Itakuwa makao ya makundi ya wanyama, wala hakuna mtu atakayewatisha. Ngome za kujihami za Efraimu zitatoweka, na utawala wa Damasko utakwisha. Waashuru ambao watabaki hai, watakuwa na fedheha kama wazawa wa Israeli. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimenena. “Siku hiyo, fahari ya Yakobo itaporomoshwa, na unono wake ataupoteza. Atakwisha kama shamba lililovunwa, atafanyiwa kama mvunaji avunavyo nafaka, atakuwa kama shamba lililovunwa bondeni Refaimu. Atabakiziwa wachache kama vile baada ya zeituni: Zeituni mbili, tatu katika tawi la juu; nne, tano katika matawi ya mti uzaao sana. Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nimenena.” Siku hiyo, watu watamwangalia Muumba wao, na kuelekeza macho yao kwa huyo Mtakatifu wa Israeli. Hawatazielekea tena madhabahu ambazo ni kazi za mikono yao wenyewe, wala kuzitazamia tena kazi za mikono yao wenyewe, yaani sanamu za mungu Ashera na madhabahu za kufukizia ubani. Siku hiyo miji yao imara itaachwa mahame, kama miji ambayo Wahivi na Waamori waliihama walipokuwa wakiwakimbia wazawa wa Israeli. Kila kitu kitakuwa uharibifu. Maana wewe Israeli umemsahau Mungu aliyekuokoa, hukumkumbuka Mwamba wa usalama wako. Kwa hiyo, hata mkipanda mimea ya Baali, na kuiweka wakfu kwa mungu wa kigeni; hata mkiifanya ikue siku hiyohiyo mliyoipanda na kuifanya ichanue asubuhi hiyohiyo, mavuno yenu yatatoweka siku hiyo ya balaa na maumivu yasiyoponyeka. Lo! Ngurumo ya watu wengi! Wananguruma kama bahari. Lo! Mlio wa watu wa mataifa! Yanatoa mlio kama wa maji mengi. Mataifa yananguruma kama ngurumo ya maji mengi, lakini Mungu atayakemea, nayo yatakimbilia mbali. Yatafukuzwa kama makapi mlimani mbele ya upepo; kama vumbi litimuliwalo na kimbunga. Wakati wa jioni yanaleta hofu kuu, lakini kabla ya asubuhi yametoweka! Hilo ndilo litakalowapata wanaonyakua mali yetu, ndilo litakalowapata wanaotupora. Ole, wake nchi iliyojaa mvumo wa mabawa, nchi iliyoko ngambo ya mito ya Kushi! Inatuma wajumbe ambao wanasafiri mtoni Nili, wamepanda mashua za mafunjo. Nendeni, enyi wajumbe wepesi, kwa taifa kubwa na hodari, la watu warefu na wa ngozi laini. Watu hao wanaoogopwa kila mahali na nchi yao imegawanywa na mito. Enyi wakazi wote ulimwenguni, nanyi mkaao duniani! Ishara itakapotolewa mlimani, tazameni! Tarumbeta itakapopigwa, sikilizeni. Maana, Mwenyezi-Mungu ameniambia hivi: “Toka makao yangu juu nitatazama yanayotukia, nimetulia kama joto katika mwanga wa jua, kama wingu la umande wakati wa mavuno. Maana, kabla ya mavuno, wakati wa kuchanua umekwisha, maua yamepukutika na kuwa zabibu mbivu, Mungu atakata chipukizi kwa kisu cha kupogolea, na kuyakwanyua matawi yanayotanda. Yote yataachiwa ndege milimani, na wanyama wengine wa porini. Ndege walao nyama watakaa humo wakati wa majira ya kiangazi, na wanyama wa porini watafanya makao humo wakati wa majira ya baridi.” Wakati huo, Mwenyezi-Mungu wa majeshi ataletewa tambiko kutoka kwa watu warefu wenye ngozi laini, watu watishao karibu na mbali, taifa la watu wenye nguvu na ushindi, ambalo ardhi yake imegawanywa na mito. Ataletewa tambiko hizo mlimani Siyoni anapoabudiwa yeye Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Kauli ya Mungu dhidi ya nchi ya Misri. “Mwenyezi-Mungu amepanda juu ya wingu liendalo kasi na kuja mpaka nchi ya Misri. Sanamu za miungu ya Wamisri zitatetemeka mbele yake, mioyo ya Wamisri itayeyuka kwa hofu. Mimi nitawachochea Wamisri wagongane: Ndugu na ndugu yake, jirani na jirani yake, mji mmoja na mji mwingine, mfalme mmoja na mfalme mwingine. Nitawaondolea Wamisri uhodari wao, nitaivuruga mipango yao; watatafuta maoni kwa sanamu na mizimu, wachawi, mizuka na pepo. Nitawatia Wamisri mikononi mwa bwana katili, mfalme mkali ambaye atawatawala. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nimenena.” Maji ya mto Nili yatakaushwa, nao utakauka kabisa. Mifereji yake itatoa uvundo, vijito vyake vitapunguka na kukauka. Nyasi na mafunjo yake yataoza. Sehemu za kandokando ya Nili zitakuwa tupu. Mimea yote iliyopandwa humo itakauka na kupeperushiwa mbali na kutoweka. Wavuvi watalia na kuomboleza, wote watumiao ndoana watalalama; wote wanaotanda nyavu majini watakufa moyo. Wafuma nguo za kitani watakata tamaa, wote kwa pamoja watakufa moyo. Wafuma nguo watafedheheshwa, na vibarua watahuzunika. Viongozi wa mji wa Soani ni wapumbavu kabisa, washauri wa Farao wanatoa shauri la kijinga! Awezaje kila mmoja kumwambia Farao, “Mimi ni mzawa wa mtaalamu stadi; mzawa wa wafalme wa hapo kale!” Wako wapi, ewe Farao, wataalamu wako? Waache basi wakuambie na kukujulisha aliyopanga Mwenyezi-Mungu wa majeshi dhidi ya Misri! Lakini viongozi wa Soani ni wapumbavu, wakuu wa Memfisi wamedanganyika. Hao walio msingi wa makabila yao wamelipotosha taifa la Misri. Mwenyezi-Mungu amewamwagia hali ya vurugu, wakawapotosha Wamisri katika mipango yao yote, wakawa kama mlevi anayeyumbayumba akitapika. Hakuna mtu yeyote nchini Misri, kiongozi au raia, mashuhuri au duni, awezaye kufanya lolote la maana. Siku ile watu wa Misri wataogopa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu watakapomwona Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameunyosha mkono wake dhidi yao. Yuda atakuwa tishio kubwa kwa Wamisri. Wote watakaoambiwa habari za Yuda wataingiwa na woga kwa sababu ya jambo aliloamua Mwenyezi-Mungu wa majeshi kuwatenda. Siku hiyo lugha ya Kiebrania itatumika katika miji mitano ya Misri, na watu wa miji hiyo wataapa kuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mji mmojawapo utaitwa “Mji wa Jua.” Siku hiyo, kutakuwa na madhabahu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu katikati ya nchi ya Misri, na nguzo iliyowekwa wakfu kwa Mungu kwenye mpaka wa Misri. Madhabahu hiyo itakuwa ishara na ushuhuda kwake Mwenyezi-Mungu wa majeshi katika nchi ya Misri. Watu wakimlilia Mwenyezi-Mungu humo kwa sababu ya kukandamizwa, yeye atawapelekea mkombozi atakayewatetea na kuwakomboa. Mwenyezi-Mungu atajijulisha kwa Wamisri na hapo ndipo Wamisri watakapomkiri na kumwabudu kwa kumtolea tambiko na sadaka za kuteketezwa. Hali kadhalika, watamwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri ambazo watazitimiza. Mwenyezi-Mungu atawaadhibu Wamisri na kuwaponya. Nao watamrudia, naye atayasikiliza maombi yao na kuwaponya. Wakati huo, kutakuwa na barabara kuu kutoka nchi ya Misri hadi nchi ya Ashuru. Waashuru watawatembelea Wamisri, na Wamisri watawatembelea Waashuru; nao wote watamwabudu Mungu pamoja. Wakati huo, Israeli itahesabiwa pamoja na Misri na Ashuru; mataifa haya matatu yatakuwa baraka kwa dunia yote. Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawabariki na kusema, “Wabarikiwe Wamisri watu wangu, kadhalika na Waashuru ambao ni ishara ya kazi yangu na Waisraeli walio mali yangu.” Sargoni mfalme wa Ashuru, alimtuma jemadari wake mkuu kuuvamia mji wa Ashdodi. Naye akaushambulia na kuuteka. Miaka mitatu kabla ya hapo, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia Isaya, mwana wa Amozi hivi: “Nenda ukavue vazi la gunia unalovaa kiunoni, na viatu miguuni mwako.” Isaya akafanya hivyo; akawa anatembea uchi na bila viatu. Basi, mnamo mwaka huo mji wa Ashdodi ulipotekwa, Mwenyezi-Mungu alisema: “Mtumishi wangu Isaya amekuwa akitembea uchi na bila viatu kwa muda wa miaka mitatu sasa, kama ishara na alama dhidi ya nchi ya Misri na Kushi. Basi, mfalme wa Ashuru atawachukua mateka Wamisri na Wakushi, wakubwa kwa wadogo. Watachukuliwa, nao watatembea uchi na bila viatu; matako wazi, kwa aibu ya Misri. Kisha wote waliotegemea Kushi na kujivunia Misri watajuta na kufadhaika. Wakati huo, wakazi wa pwani ya Filistia watasema, ‘Tazameni yaliyowapata watu tuliowategemea na kuwakimbilia kuomba msaada watuokoe na mfalme wa Ashuru! Na sasa, sisi tutawezaje kusalimika?’” Kauli ya Mungu dhidi ya jangwa kando ya bahari. Kama vimbunga vinavyovuma kutoka kusini, wavamizi wanakuja kutoka jangwani, kutoka katika nchi ya kutisha. Nimeoneshwa maono ya kutisha, maono ya watu wa hila watendao hila, maono ya watu waangamizi wafanyao maangamizi. Pandeni juu vitani enyi Waelamu; shambulieni enyi Wamedi! Mungu atakomesha mateso yote yaliyoletwa na Babuloni. Kwa maono hayo nimeingiwa na hofu kubwa, uchungu mwingi umenikumba; kama uchungu wa mama anayejifungua. Maumivu yamenizidi hata siwezi kusikia; nimefadhaika hata siwezi kuona. Moyo unanidunda na woga umenikumba. Nilitamani jioni ifike lakini ilipofika ikawa ya kutetemesha. Chakula kimetayarishwa, shuka zimetandikwa, sasa watu wanakula na kunywa. Ghafla, sauti inasikika: “Inukeni enyi watawala! Wekeni silaha tayari!” Maana Bwana aliniambia, “Nenda ukaweke mlinzi; mwambie atangaze atakachoona. Akiona kikosi, wapandafarasi wawiliwawili, wapandangamia na wapandapunda, na awe macho; naam, akae macho!” Kisha huyo mlinzi akapaza sauti: “Bwana, nimesimama juu ya mnara wa ulinzi mchana kutwa, nimeshika zamu usiku kucha!” Tazama, kikosi kinakuja, wapandafarasi wawiliwawili. Wanasema: “Babuloni umeanguka! Umeanguka! Sanamu zote za miungu yake zimetupwa chini na kuvunjwavunjwa!” Ewe Israeli, watu wangu, enyi mliotwangwa na kupurwa kama nafaka. Sasa nimewaambieni mambo niliyoyasikia kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli. Kauli ya Mungu dhidi ya Duma. Ninasikia mtu ananiita kutoka Seiri: “Mlinzi, nini kipya leo usiku? Kuna kipya chochote leo usiku?” Nami mlinzi nikajibu: “Asubuhi inakuja, kadhalika na usiku; ukitaka kuuliza, uliza tu; nenda urudi tena.” Kauli ya Mungu dhidi ya Arabia. Enyi misafara ya Dedani, pigeni kambi leo usiku kwenye nyika za Arabia. Enyi wakazi wa nchi ya Tema, wapeni maji hao wenye kiu; wapelekeeni chakula hao wakimbizi. Maana wamekimbia mapanga, mapanga yaliyochomolewa, pinde zilizovutwa na ukali wa mapigano. Maana Bwana aliniambia hivi: “Katika muda wa mwaka mmoja, bila kuzidi wala kupungua, fahari yote ya Kedari itakwisha. Wapiga upinde wachache kati ya mashujaa wa watu wa Kedari ndio watakaosalia. Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nimenena.” Kauli ya Mungu dhidi ya Bonde la Maono. Kuna nini ee Yerusalemu? Mbona watu wote mmepanda juu ya nyumba? Kwa nini mnapiga kelele za shangwe, na mji wote umechangamka na kujaa vigelegele? Watu wenu waliokufa hawakuuawa vitani, wala hawakuuawa katika mapigano. Maofisa wenu wote walikimbia, wakakamatwa hata kabla ya kufyatua mshale mmoja. Watu wako wote waliopatikana walitekwa, ingawa walikuwa wamekimbilia mbali. Ndiyo maana nawaambieni: Msijali chochote juu yangu niacheni nilie machozi ya uchungu. Msijisumbue kunifariji kwa ajili ya balaa walilopata watu wangu. Maana leo Mwenyezi-Mungu wa majeshi ametuletea mchafuko: Kushindwa na wasiwasi katika Bonde la Maono. Kuta za mji zimebomolewa, mayowe ya wakazi wake yasikika mpaka milimani. Majeshi ya Elamu, pinde na mishale mikononi, walikuja wamepanda farasi na magari ya vita; nalo jeshi la Kiri lilitayarisha ngao zake. Mabonde yako mazuri ewe Yerusalemu, yalijaa magari ya vita na farasi; wapandafarasi walijipanga tayari langoni mwako. Ulinzi wote wa Yuda uliporomoka. Siku hiyo mlikwenda kutafuta silaha zilizokuwa zimehifadhiwa katika Nyumba ya Msitu, mkaona kwamba nyufa za kuta za mji wa Daudi ni nyingi, mkajaza maji bwawa la chini. Mlizikagua nyumba za mji wa Yerusalemu, mkabomoa baadhi yake ili kupata mawe ya kuimarisha kuta za mji. Katikati ya kuta hizo mlijijengea birika la kuhifadhia maji yanapotiririka kutoka bwawa la zamani. Lakini hamkumtafuta Mungu aliyepanga mambo haya yote; hamkumjali yeye aliyepanga hayo yote tangu zamani. Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu, wa majeshi aliwataka mlie na kuomboleza, mnyoe nywele na kuvaa mavazi ya gunia. Lakini nyinyi mkafurahi na kusherehekea. Mlichinja ng'ombe na kondoo, mkala nyama na kunywa divai. Nyinyi mlisema: “Acha tule na kunywa maana kesho tutakufa.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi alinifunulia haya akisema: “Hakika hawatasamehewa uovu huu, watakufa bila kusamehewa. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliniambia niende kwa Shebna, msimamizi wa jamaa ya kifalme, nikamwambie hivi: “Una haki gani kuwa huku? Je, una ndugu yeyote hapa, hata ukajichongea kaburi mwambani juu ya mlima? Wewe ni mwenye nguvu, lakini Mwenyezi-Mungu atakutupilia mbali kwa nguvu. Atakubana kabisa na kukuzungushazungusha, kisha atakutupa kama mpira mpaka katika nchi pana. Huko utafia karibu na magari yako ya vita unayojivunia. Wewe ni aibu kwa nyumba ya bwana wako. Mwenyezi-Mungu atakungoa madarakani mwako na kukuporomosha kutoka mahali ulipo. “Siku hiyo, nitamleta mtumishi wangu Eliakimu mwana wa Hilkia. Nitamvisha vazi lako rasmi, nitamfunga mshipi wako na kumpa madaraka yako. Yeye atakuwa baba kwa watu wa Yerusalemu na kwa ukoo wa Yuda. Nitamwekea begani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Akifungua, hakuna atakayeweza kufunga na akifunga, hakuna atakayeweza kufungua. Nitamwimarisha Eliakimu kama kigingi kilichofungiwa mahali salama, naye atapata heshima tukufu katika ukoo wa wazee wake. “Watu wote na jamaa yake, wadogo kwa wakubwa watajitegemeza kwake kama chungu na vikombe vilivyotundikwa kwenye kigingi. Lakini siku moja, kama vile kile kigingi kilichofungwa mahali salama kitalegea kwa uzito, Eliakimu naye atapoteza madaraka yake na jamaa zake wote watabaki bila msaada. Mimi Mwenyezi-Mungu nimenena.” Kauli ya Mungu dhidi ya Tiro. Ombolezeni, enyi mabaharia wa mbali baharini, maana Tiro mji wenu umeharibiwa, humo hamna tena makao wala bandari. Mtazipokea habari hizo mtakaporejea kutoka Kupro. Nyamazeni kwa mshangao enyi wakazi wa pwani, naam, tulieni enyi wafanyabiashara wa Sidoni, ambao wajumbe wenu wanapita baharini, wakasafiri katika bahari nyingi. Mapato yenu yalikuwa nafaka ya Misri, mkaweza kufanya biashara na mataifa. Aibu kwako ewe Sidoni, mji wa ngome kando ya bahari! Bahari yenyewe yatangaza: “Sijapata kuwa na uchungu wa kuzaa, wala sijawahi kuzaa; sijawahi kulea wavulana, wala kutunza wasichana!” Habari zitakapoifikia Misri kwamba Tiro imeangamizwa, Wamisri watafadhaika sana. Ombolezeni enyi wenyeji wa Foinike! Jaribuni kukimbilia Tarshishi. Je, huu ndio mji wa furaha wa Tiro, mji ambao ulijengwa zamani za kale, ambao wakazi wake walikwenda kumiliki nchi za mbali? Ni nani aliyepanga mambo haya dhidi ya Tiro, mji uliowatawaza wafalme, wafanyabiashara wake walikuwa wakuu, wakaheshimiwa duniani kote? Ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi! Yeye ndiye aliyeyapanga haya yote. Alifanya hivyo akiharibu kiburi chao na kuwaaibisha waheshimiwa wake. Limeni sasa ardhi yenu enyi wakazi wa Tarshishi; maana hamna tena bandari kwa ajili ya meli kubwa. Mwenyezi-Mungu ameunyosha mkono wake juu ya bahari, amezitetemesha falme; ametoa amri kuziharibu ngome za Kanaani. Alisema: “Ewe binti Sidoni hutaweza kufanya sherehe tena; hata ukikimbilia Kupro, huko nako hutapata pumziko!” (Ni Wakaldayo, wala si Waashuru, waliowaacha wanyama wa porini wauvamie mji wa Tiro. Wao ndio waliouzungushia mji huo minara ya kuushambulia, wakayabomoa majumba yake na kuufanya magofu.) Pigeni yowe enyi meli za Tarshishi, maana kimbilio lenu limeharibiwa. Hapo mji wa Tiro utasahaulika kwa muda wa miaka sabini, muda wa maisha ya mfalme. Baada ya miaka hiyo sabini, mji wa Tiro utakumbwa na kile watu wanachoimba juu ya malaya: “Twaa kinubi chako uzungukezunguke mjini, ewe malaya uliyesahaulika! Imba nyimbo tamutamu. Imba nyimbo nyinginyingi ili upate kukumbukwa tena.” Baada ya miaka hiyo sabini, Mwenyezi-Mungu atauadhibu mji wa Tiro, nao utarudia kufanya uzinzi kwa kujiuza kwa mataifa yote ya dunia. Fedha utakayopata itawekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Mji wenyewe hautafaidika kwa fedha hiyo ila wale wanaomwabudu Mwenyezi-Mungu wataitumia kununulia chakula kingi na mavazi mazuri. Sasa Mwenyezi-Mungu anaiharibu dunia na kuifanya tupu. Atausokota uso wa dunia na kuwatawanya wakazi wake. Kila mtu atapatwa na mambo yaleyale: Mtu wa kawaida na kuhani; mtumwa na bwana wake; mjakazi na bibi yake; mnunuzi na mwuzaji; mkopeshaji na mkopaji; mdai na mdaiwa. Dunia itaharibiwa kabisa na kuangamizwa; Mwenyezi-Mungu ametamka hayo. Dunia inakauka na kunyauka; ulimwengu unafadhaika na kunyauka; mbingu zinafadhaika pamoja na dunia. Watu wameitia najisi dunia maana wamezivunja sheria za Mungu, wamezikiuka kanuni zake, wamelivunja agano lake la milele. Kwa sababu hiyo laana inaitokomeza dunia, wakazi wake wanateseka kwa makosa yao. Wakazi wa dunia wamepungua, ni watu wachache tu waliosalia. Mizabibu inanyauka, divai inakosekana. Wote waliokuwa wenye furaha sasa wanasononeka kwa huzuni. Mdundo wa vigoma umekoma, nderemo na vifijo vimetoweka; midundo ya vinubi imekomeshwa. Hakuna tena kunywa divai na kuimba; mvinyo umekuwa mchungu kwa wanywaji. Mji uliohamwa umejaa uharibifu; kila nyumba imefungwa asiingie mtu. Kuna kilio barabarani kwa kukosa divai; shangwe yote imekoma, furaha imetoweka duniani. Mji ni magofu matupu; malango yake yamevunjwavunjwa. Kama vile zeituni chache tu juu ya mzeituni au tini chache tu juu ya mtini baada ya kumaliza mavuno, ndivyo itakavyokuwa katika nchi zote: Watu wachache watabakia hai. Watakaosalia watapaza sauti, wataimba kwa shangwe. Kutoka magharibi watatangaza ukuu wa Mwenyezi-Mungu, nao wakazi wa mashariki watamsifu. Watu wa mbali watalisifu jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Tunasikia nyimbo za sifa kutoka miisho ya dunia, nyimbo za kumsifu Mungu aliye mwadilifu. Lakini mimi ninanyongonyea, naam, ninanyongonyea. Ole wangu mimi! Wasaliti wanaendelea kuwa wasaliti, usaliti wao unazidi kuwa mbaya zaidi. Hofu, mashimo na mitego, hivi ndivyo vinavyowangojeni enyi wakazi wa dunia. Atakayeikimbia hofu atatumbukia shimoni; atakayetoka shimoni atanaswa mtegoni. Madirisha ya mbinguni yamefunguliwa, misingi ya dunia inatikisika. Dunia inavunjikavunjika, inapasuka na kutikiswatikiswa. Inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda. Imelemewa na mzigo wa dhambi zake nayo itaanguka wala haitainuka tena. Siku ile Mwenyezi-Mungu ataliadhibu jeshi la angani kadhalika na wafalme wa duniani. Wote watakusanywa kama wafungwa shimoni; watafungwa gerezani pamoja kwa miaka mingi, na baada ya muda huo atawaadhibu. Kisha mwezi utaaibishwa, nalo jua litaona aibu kuangaza, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi atatawala huko Yerusalemu katika mlima Siyoni; ataonesha wazee wa watu wake utukufu wake. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe Mungu wangu; nitakutukuza na kulisifu jina lako, kwa maana umetenda mambo ya ajabu; waitekeleza kwa uaminifu na kweli mipango uliyoipanga tangu zamani. Umeufanya mji ule kuwa rundo la mawe, mji wenye ngome kuwa uharibifu. Majumba ya watu wageni yametoweka, wala hayatajengwa tena upya. Kwa hiyo watu wenye nguvu watakutukuza, miji ya mataifa katili itakuogopa. Maana wewe umekuwa ngome kwa maskini, ngome kwa fukara katika taabu zao. Wewe ni kimbilio wakati wa tufani, kivuli wakati wa joto kali. Kweli pigo la watu wakatili ni kali kama tufani inayopiga ukuta; ni kama joto la jua juu ya nchi kavu. Lakini wewe wakomesha fujo ya wageni. Kama wingu lizimavyo joto la jua ndivyo ukomeshavyo nyumba za ushindi za wakatili. Juu ya mlima Siyoni, Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawafanyia watu wote karamu ya vinono na divai nzuri, nyama tamu na mafuta, pamoja na divai safi. Katika mlima huuhuu, Mwenyezi-Mungu ataliondoa wingu la huzuni lililowafunika watu wote, kifuniko cha uchungu juu ya mataifa yote. Bwana Mungu atakiangamiza kifo milele! Atayafuta machozi katika nyuso za watu wote na kuwaondolea watu wake aibu duniani kote. Bwana Mwenyezi-Mungu ametamka. Siku ile, watu wote watasema, “Huyu ndiye Mungu wetu! Tumemngojea atuokoe. Huyu ndiye Mwenyezi-Mungu tuliyemtazamia. Njoni tufurahi na kushangilia kwa kuwa ametuokoa.” Mwenyezi-Mungu ataulinda mlima wa Siyoni, lakini watu wa Moabu watakanyagwakanyagwa nchini mwao kama nyasi katika shimo la mbolea. Watainyosha mikono yao kama mtu anayejaribu kuogelea, lakini pamoja na ustadi wao, Mwenyezi-Mungu ataporomosha kiburi chao. Atayabomoa maboma ya miji ya Moabu yenye kuta ndefu na kuyabwaga chini mavumbini. Siku ile watu wataimba wimbo huu katika nchi ya Yuda: Sisi tuna mji imara: Mungu anatulinda kwa kuta na ngome. Fungueni malango ya mji, taifa aminifu liingie; taifa litendalo mambo ya haki. Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti, wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea. Mtumaini Mwenyezi-Mungu siku zote kwa maana yeye ni mwamba wa usalama milele. Amewaporomosha waliokaa pande za juu, mji maarufu ameuangusha mpaka chini, ameutupa mpaka mavumbini. Sasa mji huo unakanyagwakanyagwa kwa miguu ya watu maskini na fukara. Njia ya watu wanyofu ni rahisi; ewe Mungu mwadilifu, wasawazisha njia yao. Katika njia ya maamuzi yako tunakungojea ee Mwenyezi-Mungu; kulikumbuka jina lako ndiyo tamaa yetu. Moyo wangu wakutamani usiku kucha, nafsi yangu yakutafuta kwa moyo. Utakapoihukumu dunia, watu wote ulimwenguni watajifunza haki. Lakini waovu hata wakipewa fadhili, hawawezi kujifunza kutenda haki. Hata katika nchi ya wanyofu, wao bado wanatenda maovu, wala hawajali ukuu wako wewe Mwenyezi-Mungu. Ee Mwenyezi-Mungu umeinua mkono kuwaadhibu, lakini maadui zako hawauoni. Waoneshe uwapendavyo watu wako nao wataaibika. Moto wa hasira yako uwateketeze maadui zako! Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umetupatia amani; umefanikisha shughuli zetu zote. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, tulipata kutawaliwa na watu wengine na miungu yao, lakini twakiri wewe pekee kuwa Mungu wetu. Watu hao wamekufa, wala hawataishi tena; wamekuwa mizimu, wala hawatafufuka. Maana wewe umewaadhibu na kuwaangamiza, hakuna atakayeweza kuwakumbuka tena. Umelikuza taifa letu, ee Mwenyezi-Mungu, naam, umelizidisha taifa letu. Umeipanua mipaka yote ya nchi, kwa hiyo wewe watukuka. Ee Mwenyezi-Mungu, walipotaabika walikutafuta, walikuomba msaada ulipowaadhibu. Kama vile mama mjamzito anayejifungua hulia na kugaagaa kwa uchungu, ndivyo tulivyokuwa kwa sababu yako, ee Mwenyezi-Mungu. Sisi tulipata maumivu ya kujifungua lakini tukajifungua tu upepo! Hatukupata ushindi wowote kwa ajili ya nchi yetu, hatukuweza kuongeza idadi ya watu katika nchi. Wafu wako wataishi tena, miili yao itafufuka. Wanaolala mavumbini wataamka na kuimba kwa furaha! Mungu atapeleka umande wake wa uhai, nao walio kwa wafu watatoka hai. Njoni watu wangu, ingieni majumbani mwenu, mkajifungie humo ndani. Jificheni kwa muda mfupi, mpaka ifike ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Maana Mwenyezi-Mungu aja kutoka kwake juu, kutoka makao yake huko mbinguni; kuwaadhibu wakazi wa dunia kwa uovu wao. Nayo dunia haitaficha tena wale waliouawa, ila itaufichua umwagaji damu wote. Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu atautwaa upanga wake mkubwa, mkali na imara, na kuliadhibu dude Lewiyathani joka lirukalo na danganyifu; Mwenyezi-Mungu ataliua joka liishilo baharini. Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu atasema hivi: “Imbeni utenzi wa shamba langu zuri la mizabibu! Mimi, Mwenyezi-Mungu, ni mkulima wake; nalimwagilia maji kila wakati, ninalilinda usiku na mchana, lisije likaharibiwa na mtu yeyote. Silikasirikii tena shamba hili; kama miiba na mbigili ingelilivamia, mimi ningepambana nayo na kuichoma moto. Maadui za watu wangu wakitaka ulinzi wangu, basi, na wafanye amani nami; naam, wafanye amani nami.” Itakuja siku wazawa wa Yakobo watashika mizizi; naam, watu wa Israeli watachanua na kuchipua, na kuijaza dunia yote kwa matunda. Mungu hakuwaadhibu Waisraeli vikali kama alivyowaadhibu maadui wake; Waisraeli waliopotea vitani, ni wachache kuliko wale wa maadui zake. Aliwaadhibu watu wake kwa kuwapeleka uhamishoni. Wakati wa upepo mkali wa mashariki, aliwaondoa kwa kipigo kikali. Hivi ndivyo uovu wa wazawa wa Yakobo utakavyoondolewa, hivi ndivyo dhambi yake itakavyofutwa kabisa: Ataziharibu madhabahu za miungu; mawe yake yatasagwasagwa kama chokaa; Ashera, wala madhabahu za kufukizia ubani hazitabaki. Mji ule wa ngome sasa umekuwa mtupu, umeachwa na kuhamwa kama jangwa, humo ndama wanalisha na kupumzika. Matawi ya miti yamekauka na kuvunjika; kina mama huyaokota wakawashia moto. Watu hawa hawajaelewa kitu, kwa hiyo Mungu, Muumba wao, hatawahurumia, yeye aliyewafanya, hatawafadhili. Siku hiyo, kutoka mto Eufrate hadi mpakani mwa Misri, Mwenyezi-Mungu ataipura nafaka yake, nanyi Waisraeli mtakusanywa mmojammoja. Siku hiyo, tarumbeta kubwa itapigwa na watu wote wa Israeli waliopotea nchini Ashuru au waliotawanywa nchini Misri watarudi na kumwabudu Mwenyezi-Mungu juu ya mlima mtakatifu huko Yerusalemu. Ole wenye majivuno na walevi wa Efraimu, fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka! Naam, fahari iliyotawala bondeni kwenye rutubarutuba; na vichwani kwao walio watu walevi kupindukia! Bwana amejichagulia mtu wake shujaa na mwenye nguvu, ambaye ni kama mvua ya mawe na dhoruba kali, kama tufani ya mafuriko makubwa; kwa mkono wake atawatupa chini ardhini. Majivuno na fahari ya walevi wa Efraimu yatakanyagwakanyagwa ardhini, fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka; fahari iliyotawala bondeni kwenye rutuba itakuwa kama tini za mwanzo kabla ya kiangazi; mtu akiziona huzichuma na kuzila mara moja. Siku ile Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuwa taji tukufu, kama kilemba kizuri kwa watu wake watakaobaki hai. Waamuzi mahakamani atawaongoza kutenda haki, nao walinzi wa mji atawapa nguvu. Lakini wako wengine waliolewa divai na kuyumbayumba kwa sababu ya pombe; naam, makuhani na manabii wamelewa mvinyo, wamevurugika kwa divai. Wanayumbayumba kwa pombe kali; maono yao yamepotoka, wanapepesuka katika kutoa hukumu. Meza zote zimetapakaa matapishi, hakuna mahali popote palipo safi. Wao wananidhihaki na kuuliza: “Huyu nabii ataka kumfundisha nani? Je, anadhani atatueleza sisi ujumbe wake? Je, sisi ni watoto wachanga walioachishwa kunyonya juzijuzi? Anatufundisha kama watoto wadogo: Sheria baada ya sheria, mstari baada ya mstari; mara hiki, mara kile!” Haya basi! Mwenyezi-Mungu ataongea na watu hawa kwa njia ya watu wa lugha tofauti wanaoongea lugha ngeni. Hata hivyo yeye alikuwa amewaahidi: “Nitawaonesheni pumziko, nitawapeni pumziko enyi mliochoka. Hapa ni mahali pa pumziko.” Lakini wao hawakutaka kunisikiliza. Kwa hiyo kwao neno la Mwenyezi-Mungu litakuwa tu: Sheria sheria, mstari mstari; mara hiki, mara kile! Nao watalazimika kukimbia lakini wataanguka nyuma; watavunjika, watanaswa na kutekwa. Basi, sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi wenye madharau mnaotawala watu wa Yerusalemu, “Nyinyi mnajidai mmefanya mkataba na kifo, mmefanya mapatano na Kuzimu! Nyinyi mwasema eti balaa lijapo halitawapata, kwa sababu mmefanya uongo kuwa tegemeo lenu, na udanganyifu kuwa kinga yenu!” Basi, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu: “Tazama! Naweka mjini Siyoni jiwe la msingi, jiwe ambalo limethibitika. Jiwe la pembeni, la thamani, jiwe ambalo ni la msingi thabiti; jiwe lililo na maandishi haya: ‘Anayeamini hatatishika.’ Nitatumia haki kama kipimo changu, nitatumia uadilifu kupimia.” Mvua ya mawe itaufagilia mbali uongo mnaoutegemea, na mafuriko yataharibu kinga yenu. Hapo mkataba wenu na kifo utabatilishwa, na mapatano yenu na Kuzimu yatafutwa. Janga lile kuu litakapokuja litawaangusheni chini. Kila litakapopitia kwenu litawakumba; nalo litapita kila asubuhi, mchana na usiku. Kusikia ujumbe huu tu kutakuwa kitisho. Kwenu itakuwa kama ajinyoshaye juu ya kitanda kifupi mno, au kujifunika kwa blanketi lililo dogo mno! Maana Mwenyezi-Mungu atainuka kama kule mlimani Perazimu; atawaka hasira kama kule bondeni Gibeoni. Atatekeleza mpango wake wa ajabu; atatenda kazi yake ya kustaajabisha. Basi, nyinyi msiwe na madharau vifungo vyenu visije vikakazwa zaidi. Maana nimesikia kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameazimia kuiangamiza nchi yote. Tegeni sikio msikilize ninayowaambieni; sikilizeni kwa makini hotuba yangu. Je, alimaye ili kupanda hulima tu? Je, huendelea kulima na kusawazisha shamba lake? La! Akisha lisawazisha shamba lake, hupanda mbegu za bizari na jira, akapanda ngano na shayiri katika safu, na mipakani mwa shamba mimea mingineyo. Mtu huyo huwa anajua la kufanya, kwa sababu Mungu wake humfundisha. Bizari haipurwi kwa mtarimbo wala jira kwa gari la ng'ombe! Ila bizari hupurwa kwa kijiti na jira kwa fimbo. Mkulima apurapo ngano yake, haendelei kuipura mpaka kuvunja punje zake. Anajua jinsi ya kuipura kwa gurudumu, bila kuziharibu punje za ngano. Ujuzi huu nao watoka kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mipango yake Mungu ni ya ajabu, hekima yake ni kamilifu kabisa. Ole wako Yerusalemu, madhabahu ya Mungu; mji ambamo Daudi alipiga kambi yake! Miaka yaja na kupita, na sikukuu zako zaendelea kufanyika; lakini mimi Mungu nitauhuzunisha Yerusalemu, nako kutakuwa na vilio na maombolezo, mji wenyewe utakuwa kama madhabahu iliyolowa damu ya watu waliouawa. Mimi nitapanga jeshi dhidi ya Yerusalemu, nami nitauzingira na kuushambulia. Utaangushwa mbali sana ndani ya ardhi; kutoka huko mbali utatoa sauti; maneno yako yatatoka huko chini mavumbini; sauti yako itatoka ardhini kama ya mzimu. Kundi la maadui zako litakuwa kama vumbi laini, waliokutendea ukatili watakuwa kama makapi. Hayo yatafanyika ghafla. Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuja kukusaidia; atakuja na ngurumo, tetemeko la ardhi na sauti kubwa; atakuja na kimbunga, tufani na moto uunguzao. Hapo, kundi la mataifa yote yanayoshambulia Yerusalemu, wote wanaoshambulia ngome yake na kuutia wasiwasi, watatoweka kama ndoto, kama maono ya usiku. Mataifa yote yanayoushambulia mji wa Yerusalemu yatakuwa kama mtu mwenye njaa anayeota anakula lakini aamkapo bado anaumwa na njaa! Au mtu mwenye kiu anayeota kuwa anakunywa, lakini anaamka mdhaifu, bado ana kiu. Endeleeni kuwa wapumbavu na kuduwaa! Jipofusheni na kuwa vipofu! Leweni lakini si kwa divai; pepesukeni lakini si kwa pombe. Mwenyezi-Mungu amewamiminia hali ya usingizi mzito; ameyafumba macho yenu enyi manabii, amefunika vichwa vyenu enyi waonaji. Basi, kwenu nyinyi maono yote haya ni kama ujumbe ulioandikwa katika kitabu kilichofungwa kwa mhuri. Ukimpelekea mtu yeyote ajuaye kusoma, ukamwambia, “Hebu nisomee kitabu hiki,” atasema, “Siwezi kukisoma kwani kimefungwa kwa mhuri.” Na ukimpa mtu yeyote asiyejua kusoma, ukamwambia, “Hebu nisomee kitabu hiki,” atakuambia, “Sijui kusoma.” Bwana asema, “Watu hawa huja kuniabudu kwa maneno matupu, hali mioyo yao iko mbali nami. Wananiheshimu kulingana na mapokeo ya watu tu, jambo walilojifunza wao wenyewe. Hivyo, nitawatenda tena watu hawa maajabu, mambo ya ajabu na ya kushangaza. Nao wenye hekima wao wataishiwa hekima, na busara ya wenye busara wao itatoweka. “Ole mnaomficha Mwenyezi-Mungu mipango yenu, mnaotenda matendo yenu gizani na kusema: ‘Hamna atakayetuona; nani awezaye kujua tunachofanya?’ Nyinyi mnafanya mambo kinyume kabisa! Je, mfinyanzi na udongo ni hali moja? Chombo hakiwezi kumwambia aliyekitengeneza: ‘Wewe hukunitengeneza.’ Kilichofinyangwa hakiwezi kumwambia aliyekiumba, ‘Wewe hujui chochote.’” Bado kidogo tu, msitu wa Lebanoni utageuzwa kuwa shamba lenye rutuba, na shamba lenye rutuba kuwa msitu. Siku hiyo viziwi watasikia ujumbe ukisomwa kitabuni na kutoka gizani vipofu wataanza kuona. Wanyofu watapata furaha mpya kwa Mwenyezi-Mungu, na maskini wa watu watashangilia kwa furaha kwa sababu ya Mungu, Mtakatifu wa Israeli. Majitu makatili yataangamizwa, wenye kumdhihaki Mungu watakwisha, wote wanaootea kutenda maovu watatokomezwa. Watatoweka wale wanaopotosha kesi ya mtu mahakamani, watu wanaowafanyia hila mahakimu na wasemao uongo kuwanyima haki yao wasio na hatia. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu aliyemkomboa Abrahamu, asema hivi kuhusu wazawa wa Yakobo: “Wazawa wa Yakobo hawataaibishwa tena, hawatainamisha vichwa vyao tena kwa aibu. Watakapowaona watoto wao, watoto niliowajalia mimi mwenyewe, watalitukuza jina langu mimi Mtakatifu wa Yakobo; watakuwa na uchaji kwangu mimi Mungu wa Israeli. Waliopotoka rohoni watapata maarifa na wenye kununa watakubali kufunzwa.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ole wao watoto wanaoniasi, wanaotekeleza mipango yao na si mipango yangu, wanaofanya mikataba kinyume cha matakwa yangu! Naam, wanarundika dhambi juu ya dhambi. Bila kunitaka shauri, wanafunga safari kwenda Misri, kukimbilia usalama katika ulinzi wa Farao, kupata mahali pa usalama nchini Misri. Lakini ulinzi wa Farao utakuwa aibu yenu, na usalama nchini Misri utakuwa fedheha yenu. Maana ingawa maofisa wao wamefika Soani, na wajumbe wao mpaka Hanesi, wote wataaibishwa na hao wasioweza kuwasaidia, watu ambao hawawezi kuwapa msaada au faida, ila tu kuwapa aibu na fedheha.” Kauli ya Mungu juu ya wanyama wa pande za Negebu: “Wajumbe wanapita katika nchi ya taabu na shida, yenye simba, nyoka wa sumu na majoka. Wamewabebesha wanyama wao mali zao, kuwapelekea watu wasioweza kuwafaa kitu. Maana msaada wa Misri ni bure, haufai kitu; kwa hiyo nimeipanga Misri jina: ‘Joka lisilo na nguvu!’” Mungu aliniambia: “Sasa chukua kibao cha kuandikia, uandike jambo hili mbele yao, liwe ushahidi wa milele: Watu hawa ni waasi, watoto wasioaminika; watu wasiopenda kusikia mafunzo ya Mwenyezi-Mungu. Huwaambia waonaji: ‘Msione maono’, na manabii: ‘Msitutangazie ukweli, bali tuambieni mambo ya kupendeza, toeni unabii wa mambo ya udanganyifu tu. Geukeni na kuiacha njia ya ukweli; msituambie tena juu ya Mungu, Mtakatifu wa Israeli.’” Kwa hiyo Mungu, Mtakatifu wa Israeli asema: “Nyinyi mmeukataa ujumbe wangu; mkapania kufanya dhuluma na udanganyifu. Basi, dhambi hii itawaleteeni maangamizi kama ufa mkubwa katika ukuta mrefu; utabomoka mara na kuanguka chini ghafla. Kuporomoka kwa ukuta huo, ni kama kupasuka kwa chungu ambacho kimepasuliwa vibaya sana, bila kusalia kigae cha kuchukulia moto mekoni, au kuchotea maji kisimani.” Bwana Mungu, Mtakatifu wa Israeli, asema: “Mkinirudia na kutulia mtaokolewa; kwa utulivu na kunitumainia mtapata nguvu.” Lakini nyinyi hamkutaka. Badala yake mlisema, “La! Sisi tutakimbia na farasi wenye mbio.” Sawa, mtakimbia na farasi wenye mbio, lakini farasi wa maadui zenu wana mbio zaidi. Watu wenu elfu moja watamkimbia askari mmoja adui; na askari watano maadui watawakimbizeni nyote. Mwishowe, watakaosalia watakuwa kama mlingoti wa bendera mlimani, kama alama iliyo juu ya kilima. Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu anangoja awafadhili, atainuka na kuwaonea huruma. Maana, Mwenyezi-Mungu ni Mungu atendaye haki. Heri wote wale wanaomtumainia. Enyi watu wa Siyoni, enyi watu wa Yerusalemu, hakika nyinyi hamtaomboleza tena. Kweli Mungu atawahurumia; mara tu atakaposikia kilio chenu atawaitikeni. Ingawa Bwana atawalisha taabu na kuwanywesha dhiki, yeye ndiye Mwalimu wenu na hatajificha tena; nanyi mtamwona kwa macho yenu wenyewe. Mkienda kulia au kushoto, mtasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Njia ni hii; ifuateni.” Mtavifanya haramu vinyago vyenu vya miungu vilivyopakwa fedha na sanamu zenu zilizopakwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitu najisi, mkisema, “Poteleeni mbali!” Mtakapopanda mbegu zenu, Mwenyezi-Mungu atanyesha mvua kwa wakati wake, nazo zitakua na kuwapa mavuno mengi. Mifugo yenu nayo itapata malisho kwa wingi. Mafahali na punda wenu wa kulimia watapata malisho yaliyochambuliwa vizuri na kutiwa chumvi. Wakati utakapofika ambapo maadui watauawa na ngome zao kubomolewa, vijito vya maji vitatiririka kutoka kila mlima na kilima. Tena mwezi utawaka kama jua, nao mwanga wa jua utakuwa mara saba ya mwanga wake wa kawaida, kana kwamba mwanga wa siku saba umeangaza katika siku moja. Mambo haya yote yatatukia wakati Mwenyezi-Mungu atakapoyafunga na kuyaponya majeraha aliyowaletea watu wake. Tazameni, Mwenyezi-Mungu mwenyewe anakuja toka mbali! Amewaka hasira na moshi wafuka; midomo yake yaonesha ghadhabu yake, maneno anayosema ni kama moto uteketezao. Pumzi yake ni kama mafuriko ya mto ambao maji yake yanafika hadi shingoni. Anakuja kuyachekecha mataifa kwa chekecheke ya maangamizi, kuwafunga lijamu na kuwapeleka wasikotaka. Lakini nyinyi watu wa Yerusalemu mtaimba kwa furaha kama mfanyavyo wakati wa mkesha wa sikukuu. Mtajaa furaha kama watu wanaotembea kwa mdundo wa muziki wa filimbi kwenda mlimani kwa Mwenyezi-Mungu, Mwamba wa Israeli. Mwenyezi-Mungu atawafanya watu wote waisikie sauti yake tukufu na pigo la nguvu yake lionekane kwa hasira nyingi. Kutakuwa na ndimi za moto mkali, ngurumo, dhoruba na mvua ya mawe. Waashuru watajaa hofu watakaposikia sauti ya Mwenyezi-Mungu wakati atakapowachapa na fimbo yake. Kila pigo la adhabu ya Mwenyezi-Mungu juu ya Waashuru litaandamana na mdundo wa ngoma na zeze. Yeye mwenyewe binafsi atapigana na Waashuru. Naam, mahali pa kumteketeza mfalme wa Ashuru pamekwisha tayarishwa muda mrefu uliopita. Mahali penyewe ni shimo kubwa na pana. Moto upo na kuni kwa wingi. Mwenyezi-Mungu ataupulizia pumzi yake kama kijito cha madini ya kiberiti na kuuwasha. Ole wao wale waendao Misri kuomba msaada, ole wao wanaotegemea farasi, wanaotegemea wingi wa magari yao ya vita, na nguvu za askari wao wapandafarasi, nao hawamtegemei Mtakatifu wa Israeli, wala hawamwombi Mwenyezi-Mungu shauri! Mungu ni mwenye busara na huleta maangamizi. Habadilishi tamko lake; ila yuko tayari kuwakabili watu waovu kadhalika na wasaidizi wa watendao mabaya. Wamisri ni binadamu tu wala si Mungu; farasi wao nao ni wanyama tu, si roho. Mwenyezi-Mungu akiunyosha mkono wake, taifa linalotoa msaada litajikwaa, na lile linalosaidiwa litaanguka; yote mawili yataangamia pamoja. Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Kama vile simba au mwanasimba angurumavyo kuyakinga mawindo yake, hata kundi la wachungaji likiitwa kumkabili, yeye hatishiki kwa kelele zao, wala hashtuki kwa sauti zao. Ndivyo atakavyoshuka Mwenyezi-Mungu wa majeshi kupigana juu ya mlima Siyoni na kilima chake. Kama ndege arukavyo juu ya viota vyake, ndivyo Mwenyezi-Mungu atakavyoulinda Yerusalemu, ataulinda na kuukomboa, atauhifadhi na kuuokoa. Enyi Waisraeli, mrudieni huyo mliyemsaliti vibaya. Wakati utafika ambapo nyote mtavitupilia mbali vinyago vyenu vya fedha na dhahabu ambavyo mmejitengenezea kwa mikono yenu, vikawakosesha. Hapo Waashuru watauawa kwa upanga, lakini si kwa upanga wa binadamu; naam, wataangamizwa kwa upanga ambao ni zaidi ya ule wa binadamu. Waashuru watakimbia na vijana wao watafanyizwa kazi za kitumwa. Mfalme wao atatoroka kwa hofu, na maofisa wao wataiacha bendera yao kwa woga. Hayo ameyatamka Mwenyezi-Mungu ambaye moto wake umo mjini Siyoni, naam, tanuri lake limo mjini Yerusalemu.” Kutatokea mfalme atakayetawala kwa uadilifu, nao viongozi wataongoza kwa kufuata haki. Kila mmoja atakuwa kama mahali pa kujikinga na upepo, kama mahali pa kujificha wakati wa tufani. Watakuwa kama vijito vya maji katika nchi kame, kama kivuli cha mwamba mkubwa jangwani. Macho hayatafumbwa tena, masikio yatabaki wazi. Wafanyao mambo kwa hamaki wataamua kwa busara, wenye kigugumizi wataongea sawasawa. Wapumbavu hawataitwa tena waungwana, wala walaghai hawataitwa tena waheshimiwa. Wapumbavu hunena upumbavu, na fikira zao hupanga kutenda uovu, kutenda mambo yasiyo mema, kusema mambo ya kumkufuru Mwenyezi-Mungu. Huwaacha wenye njaa bila chakula, na wenye kiu huwanyima kinywaji. Ulaghai wa walaghai ni mbaya; hao huzua visa viovu, na kumwangamiza maskini kwa maneno ya uongo, hata kama madai ya maskini ni halali. Lakini waungwana hutenda kiungwana, nao hutetea mambo ya kiungwana. Inukeni, enyi wanawake mnaostarehe, mnisikilize; sikilizeni ninayosema enyi mabinti mlioridhika. Katika mwaka mmoja hivi mtatetemeka nyinyi mliotosheka; maana hamtapata mavuno yoyote, na mavuno ya zabibu yatatoweka. Tetemekeni kwa woga, enyi mnaojikalia tu; tetemekeni kwa hofu, enyi mnaostarehe! Vueni nguo zenu, mbaki uchi, mjifunge vazi la gunia viunoni mwenu. Jipigeni vifua kwa huzuni, ombolezeni, kwa sababu ya bustani zilizokuwa nzuri, kwa mizabibu iliyokuwa ikizaa sana, kwa ardhi ya watu wangu inayoota miiba na mbigili, kwa nyumba zote zilizojaa watu wenye furaha, kwa mji uliokuwa na shangwe. Maana ikulu ya mfalme itaachwa mahame, mji huo wa watu wengi utahamwa. Mlima na mnara wa ulinzi utakuwa mapango milele, pundamwitu watapitapita huko kwa furaha, kondoo watapata malisho yao humo. Hali itaendelea kuwa hivyo mpaka tumiminiwe roho ya Mungu kutoka juu. Hapo jangwa litakuwa shamba la rutuba tena, na mashamba ya rutuba yatakuwa msitu. Haki itadumu katika nchi iliyokuwa nyika, uadilifu utatawala katika mashamba yenye rutuba. Kutokana na uadilifu watu watapata amani, utulivu na usalama utadumu milele. Watu wangu watakaa katika makao ya amani, katika maskani salama na mazingira matulivu. Msitu wa adui utatoweka kabisa, na mji wake utaangamizwa. Lakini heri yenu nyinyi: Mtapanda mbegu zenu popote penye maji, ng'ombe na punda wenu watatembeatembea watakavyo. Ole wako ewe mwangamizi, unayeangamiza bila wewe kuangamizwa! Ole wako wewe mtenda hila, ambaye hakuna aliyekutendea hila! Utakapokwisha kuangamiza wewe utaangamizwa! Utakapomaliza kuwatendea watu hila wewe utatendewa hila. Ee Mwenyezi-Mungu, utuonee huruma, kwako tumeliweka tumaini letu. Uwe kinga yetu kila siku, wokovu wetu wakati wa taabu. Kwa kishindo cha sauti yako watu hukimbia; unapoinuka tu, mataifa hutawanyika. Maadui zao wanakusanya mateka, wanayarukia kama panzi. Mwenyezi-Mungu ametukuka, yeye anaishi juu mbinguni. Ameujaza Siyoni haki na uadilifu. Enyi watu wa Yerusalemu, Mwenyezi-Mungu atawajalieni usalama, atawaokoa na kuwapa hekima na maarifa. Hazina yenu kuu ni kumcha Mwenyezi-Mungu. Haya, mashujaa wao wanalia, wajumbe wa amani wanaomboleza. Barabara kuu zimebaki tupu; hamna anayesafiri kupitia humo. Mikataba inavunjwa ovyo, mashahidi wanadharauliwa. Hamna anayejali tena maisha ya binadamu. Nchi inaomboleza na kunyauka; misitu ya Lebanoni imekauka, bonde zuri la Sharoni limekuwa jangwa, huko Bashani na mlimani Karmeli miti imepukutika majani yake. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Sasa mimi nitainuka; sasa nitajiweka tayari; sasa mimi nitatukuzwa. Mipango yenu yote ni kama makapi, na matokeo yake ni takataka tupu. Pumzi yangu itawaangamiza kama moto. Watu watakuwa kama wamechomwa kuwa majivu, kama miiba iliyokatwa na kuteketezwa motoni. Sikilizeni mambo mliyofanya enyi mlio mbali, nanyi mlio karibu kirini uwezo wangu.” Wenye dhambi katika Siyoni wanaogopa, wasiomcha Mungu wanatetemeka na kusema: “Nani awezaye kuukaribia moto huu mkali? Nani awezaye kustahimili miali ya moto wa milele?” Ni mtu aishiye kwa uadilifu na asemaye ukweli; mtu anayedharau kabisa utajiri wa dhuluma, anayekataa hongo kata kata, asiyekubali kamwe kusikia mipango ya mauaji, wala hakubali macho yake yaone maovu. Mtu wa namna hiyo anaishi juu, mahali salama penye ngome na miamba; chakula chake atapewa daima, na maji yake ya kunywa hayatakosekana. Mtaweza kumwona mfalme katika fahari yake, mtaiona nchi anayotawala, kubwa na pana. Mtafikiria tisho lililopita na kujiuliza, “Wako wapi wale waliokadiria na kukisia kodi? Wako wapi wale waliopeleleza ulinzi wetu?” Hamtawaona tena watu wale wenye kiburi, wanaozungumza lugha isiyoeleweka. Tazameni Siyoni tunamofanya sikukuu zetu; tazameni mji Yerusalemu, makao matulivu, hema imara; vigingi vyake havitangolewa kamwe, kamba zake hazitakatwa hata moja. Humo Mwenyezi-Mungu atatuonesha ukuu wake. Kutakuwa na mito mikubwa na vijito, ambamo meli za vita hazitapita, wala meli kubwa kuingia. Maana Mwenyezi-Mungu ni hakimu wetu, yeye ni mtawala wetu; Mwenyezi-Mungu ni mfalme wetu, yeye ndiye anayetuokoa. Ewe Siyoni, kamba zako zimelegea, haziwezi kushikilia matanga yake, wala kuyatandaza. Lakini nyara nyingi zitagawanywa; hata vilema wataweza kuchukua sehemu yao. Hakuna atakayesema tena ni mgonjwa; watu watasamehewa uovu wao wote. Karibieni mkasikilize enyi mataifa, tegeni sikio enyi watu. Sikiliza ee dunia na vyote vilivyomo, ulimwengu na vyote vitokavyo humo! Mwenyezi-Mungu ameyakasirikia mataifa yote, ameghadhabika dhidi ya majeshi yao yote. Ameyapangia mwisho wao, ameyatoa yaangamizwe. Maiti zao zitatupwa nje; harufu ya maiti zao itasambaa; milima itatiririka damu yao. Jeshi lote la angani litaharibika, anga zitakunjamana kama karatasi. Jeshi lake lote litanyauka, kama majani ya mzabibu yanyaukavyo, naam, kama tunda la mtini linyaukavyo. Upanga wa Mungu uko tayari juu mbinguni. Tazama, washuka kuwaadhibu Waedomu, watu ambao ameamua kuwaangamiza. Upanga utalowa damu na kutapakaa mafuta, kama kwa damu ya kondoo na mbuzi, na mafuta ya figo za kondoo dume. Maana Mwenyezi-Mungu atatoa kafara huko Bosra, kutakuwa na mauaji makubwa nchini Edomu. Nyati wataangamia pamoja nao, ndama kadhalika na mafahali. Nchi italoweshwa damu, udongo utarutubika kwa mafuta yao. Maana Mwenyezi-Mungu anayo siku ya kisasi; mwaka wa kulipiza maadui wa Siyoni. Vijito vya Edomu vitatiririka lami, udongo wake utakuwa madini ya kiberiti; ardhi yake itakuwa lami iwakayo. Itawaka usiku na mchana bila kuzimika, moshi wake utafuka juu milele. Nchi itakuwa jangwa siku zote, hakuna atakayepitia huko milele. Itakuwa makao ya kozi na nungunungu, bundi na kunguru wataishi humo. Mwenyezi-Mungu atawaletea ghasia, na timazi la fujo kwa wakuu wake. Nchi itaitwa “Nchi bila Mfalme;” wakuu wake wote wametoweka. Miiba itaota katika ngome zake, viwavi na michongoma mabomani mwao. Itakuwa makao ya mbwamwitu, maskani yao mbuni. Pakamwitu na fisi watakuwa humo, majini yataitana humo; kwao usiku utakuwa mwanga, na humo watapata mahali pa kupumzikia. Humo bundi watataga mayai na kuyaatamia, wataangua vifaranga na kuviweka kivulini mwao. Humo vipanga watakutania, kila mmoja na mwenzake. Someni katika kitabu cha Mwenyezi-Mungu: “Hakuna hata kiumbe kimoja kitakachokosekana, kila kimoja kitakuwako na mwenzake.” Maana Mwenyezi-Mungu mwenyewe ametamka hivyo, roho yake itawakusanya hao wote. Mwenyezi-Mungu amepanga sehemu ya kila mmoja wao, ametumia kamba kuwapimia nchi hiyo; wataimiliki milele na milele, wataishi humo kizazi hata kizazi. Nyika na nchi kavu vitachangamka, jangwa litafurahi na kuchanua maua. Litachanua maua kwa wingi kama waridi, litashangilia na kuimba kwa furaha. Mungu atalijalia fahari ya milima ya Lebanoni, uzuri wa mlima Karmeli na wa bonde la Sharoni. Watu watauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu, watauona ukuu wa Mungu wetu. Imarisheni mikono yenu dhaifu, kazeni magoti yenu manyonge. Waambieni waliokufa moyo: “Jipeni moyo, msiogope! Tazameni Mungu wenu atakuja kulipiza kisasi, atakuja kuwaadhibu maadui zenu; atakuja yeye mwenyewe kuwaokoeni.” Hapo vipofu wataona tena, na viziwi watasikia tena. Walemavu watarukaruka kama paa, na bubu wataimba kwa furaha. Maji yatabubujika nyikani na vijito vya maji jangwani. Mchanga wa moto jangwani utakuwa bwawa la maji, ardhi kavu itabubujika vijito vya maji. Makao ya mbwamwitu yatajaa maji; nyasi zitamea na kukua kama mianzi. Humo kutakuwa na barabara kuu, nayo itaitwa “Njia Takatifu.” Watu najisi hawatapitia humo, ila tu watu wake Mungu; wapumbavu hawatadiriki kuikanyaga, humo hakutakuwa na simba, mnyama yeyote mkali hatapitia humo, hao hawatapatikana humo. Lakini waliokombolewa ndio watakaopita humo. Waliokombolewa na Mwenyezi-Mungu watarudi, watakuja Siyoni wakipiga vigelegele. Watakuwa wenye furaha ya milele, watajaliwa furaha na shangwe; huzuni na kilio vitatoweka kabisa. Mnamo mwaka wa kumi na nne wa utawala wa mfalme Hezekia, mfalme Senakeribu wa Ashuru aliishambulia miji yote yenye ngome ya Yuda na kuiteka. Kisha mfalme wa Ashuru alimtuma jemadari mkuu kutoka Lakishi na jeshi kubwa kumwendea mfalme Hezekia. Jemadari alisimama karibu na mfereji wa bwawa lililoko upande wa juu katika barabara kuu inayoelekea uwanda wa Dobi. Nao walilakiwa na Eliakimu mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa ikulu, Shebna aliyekuwa katibu, pamoja na mwandishi Yoa mwana wa Asafu. Ndipo mkuu wa matowashi wa Ashuru alipowaambia, “Mwambieni Hezekia kuwa mfalme mkuu wa Ashuru anamwuliza, ‘Je, unategemea nini kwa ukaidi wako huo? Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi? Angalia! Sasa unategemea Misri, utete uliovunjika ambao utamchoma mkono yeyote atakayeuegemea. Hivyo ndivyo Farao, mfalme wa Misri alivyo, kwa wote wale wanaomtegemea.’ Lakini hata kama mkiniambia, ‘Tunamtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,’ je, si huyohuyo ambaye Hezekia aliziharibu madhabahu zake na kuwaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, ‘Mnapaswa kuabudu mbele ya madhabahu hii?’ Basi, fanyeni mkataba na bwana wangu mfalme wa Ashuru; mimi nitawapatieni farasi 2,000, kama mtaweza kupata wapandafarasi. Mwawezaje kumrudisha nyuma ofisa mmoja kati ya watumishi wa bwana wangu aliye na cheo cha chini sana wakati mnategemea Misri kupata magari ya vita na wapandafarasi! Zaidi ya hayo, je, mnafikiri nimekuja bila amri ya Mwenyezi-Mungu ili kuishambulia na kuiangamiza nchi hii? Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeniambia ‘Ishambulie nchi hii na kuiangamiza!’” Kisha Eliakimu, Shebna na Yoa wakamjibu mkuu wa matowashi, “Tafadhali sema nasi kwa lugha ya Kiaramu maana tunaielewa. Usiseme nasi kwa lugha ya Kiebrania kwa kuwa watu walioko ukutani wanasikia.” Yule mkuu wa matowashi akawaambia, “Je unadhani bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu wenyewe tu? Maneno yangu ni pia kwa watu wanaokaa ukutani! Muda si muda wao kama vile nyinyi itawabidi kula mavi yao wenyewe na kunywa mikojo yao wenyewe!” Kisha huyo mkuu wa matowashi akasimama, akapaza sauti na kusema kwa Kiebrania, “Sikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! Hiki ndicho anachosema mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye, kwa sababu hataweza kuwaokoa. Msikubali awashawishi ili mumtegemee Mwenyezi-Mungu akisema, ‘Mwenyezi-Mungu hakika atatuokoa na mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’ Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru anasema: ‘Muwe na amani nami, na kujisalimisha kwangu. Hapo kila mmoja wenu ataweza kula matunda ya mzabibu wake mwenyewe na ya matunda ya mtini wake mwenyewe na kunywa maji ya kisima chake mwenyewe. Mpaka baadaye nitakapokuja na kuwapelekeni katika nchi kama hii yenu; nchi yenye nafaka na divai, nchi yenye mkate na mashamba ya mizabibu.’ Angalieni basi Hezekia asiwahadae akisema kwamba Mwenyezi-Mungu atawaokoeni. Je, kuna yoyote kati ya miungu ya mataifa aliyewahi kuokoa nchi yake mkononi mwa mfalme wa Ashuru? Je, iko wapi miungu ya Hamathi na Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu? Je, imeokoa Samaria mkononi mwangu? Ni nani miongoni mwa miungu ya nchi hizi aliyeokoa nchi zao katika mkono wangu, hata iwe kwamba Mwenyezi-Mungu ataweza kuuokoa mji wa Yerusalemu mkononi mwangu?” Lakini watu walinyamaza, wala hawakumjibu neno kama vile walivyoamriwa na mfalme akisema, “Msimjibu.” Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa mkuu wa ikulu, katibu Shebna, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi, wakamwendea mfalme Hezekia huku mavazi yao yakiwa yameraruliwa, wakamweleza maneno ya mkuu wa matowashi. Basi, mfalme Hezekia aliposikia habari hiyo alirarua mavazi yake, akavaa vazi la gunia, akaingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia. Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa, na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama anayetaka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa. Inawezekana kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya mkuu wa matowashi ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atapinga maneno aliyoyasikia; kwa hiyo waombee watu waliobaki.’” Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya, yeye akawaambia, “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Usiogope kwa sababu ya maneno ya watumishi wa mfalme wa Ashuru uliyoyasikia, maneno ambayo wameyasema kunidharau. Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi halafu atarudi katika nchi yake, na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’” Kisha yule mkuu wa matowashi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akishambulia mji wa Libna. Halafu aliposikia habari kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi anakuja kupigana naye, alituma wajumbe kwa Hezekia, akisema, “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru. Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, unadhani wewe utaokoka? Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo wazee wangu waliyaangamiza? Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na Iva?’” Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema; “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, unayeketi katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa. Wewe ndiwe uliyeumba mbingu na dunia. Ee, Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka na kukutukana wewe Mungu uliye hai. Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa yote na nchi zao. Waliweza kuitupa miungu yao motoni, kwa sababu haikuwa miungu kweli bali sanamu za miti au mawe zilizochongwa na mikono ya watu. Sasa ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, utuokoe makuchani mwa Senakeribu, ili falme zote za dunia zijue kwamba wewe peke yako ndiwe uliye Mwenyezi-Mungu.” Kisha Isaya mwana na Amozi, alituma ujumbe kwa Hezekia akisema, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: Kwa kuwa umeniomba kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru, basi huu ndio ujumbe wangu kuhusu huyo mfalme: Mji wa Siyoni, naam, Yerusalemu, unakudharau na kukutukana. Yerusalemu, mji mzuri unakutikisia kichwa kwa dhihaka. Wewe umemtukana nani? Umemkashifu nani? Umethubutu kumbeza nani kwa majivuno? Ni mimi Mungu, Mtakatifu wa Israeli! Umewatumia watumishi wako kunidhihaki mimi Bwana; wewe umesema, ‘Kwa magari yangu mengi ya vita, nimekwea vilele vya milima, mpaka kilele cha Lebanoni. Nimeangusha mierezi yake mirefu, na misonobari mizurimizuri. Nimevifikia vilele vyake na ndani ya misitu yake mikubwa. Nimechimba visima na kunywa maji yake, na nilikausha vijito vya Misri kwa nyayo za miguu yangu.’ “Je, hujasikia ewe Senakeribu kwamba nilipanga jambo hili tangu zamani? Ninachotekeleza sasa nilikipanga zamani. Nilikuweka uifanye miji yenye ngome kuwa rundo la magofu. Wakazi wake wakiwa wameishiwa nguvu, wametishika na kufadhaika. Wamekuwa kama mimea shambani, kama nyasi changa shambani, kama majani yaotayo juu ya paa au kama ngano kabla hazijakomaa ambazo hunyauka upepo mkavu uvumapo. Lakini, nakujua wewe Senakeribu; najua kila unachofanya na kuacha kufanya; najua mipango yako dhidi yangu. Kwa vile umefanya mipango dhidi yangu na nimeusikia ufidhuli wako, nitatia ndoana yangu puani mwako, na lijamu yangu kinywani mwako. Nitakurudisha njia ileile uliyojia.” “Na hii ndiyo itakuwa ishara kwako Hezekia: Mwaka huu na mwaka ujao mtakula kinachomea chenyewe bila kupandwa. Lakini katika mwaka wa tatu mtapanda na kuvuna mavuno; mtapanda mizabibu na kula matunda yake. Wale watakaobaki katika ukoo wa Yuda wataongezeka na kuwa wengi kama vile mti unavyotoa mizizi yake udongoni na kuzaa matunda juu. Maana kutakuwa na watu watakaosalia huko Yerusalemu; naam, huko mlimani Siyoni kutakuwako watu wachache watakaosalimika.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amedhamiria kukamilisha hayo. Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu, wala kuupiga mshale wala kuingia kwa ngao wala kuuzingira. Atarudi kwa njia ileile aliyojia na wala hataingia katika mji huu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimetamka hayo. Naam, kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi nitaulinda na kuuokoa mji huu.” Basi, wakati wa usiku malaika wa Mwenyezi-Mungu aliingia kambini mwa Waashuru na kuwaua watu 185,000. Halafu kulipopambazuka watu hao wote walionekana wakiwa maiti. Kisha Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda kwake, akakaa Ninewi. Siku moja, wakati Senakeribu alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki mungu wake, wanawe wawili, Adrameleki na Sharezeri, walimuua kwa upanga, halafu wakakimbilia nchini Ararati. Naye Esar-hadoni, mwanawe, akatawala badala yake. Wakati huo, mfalme Hezekia aliugua sana karibu kufa. Ndipo nabii Isaya mwana wa Amozi, akamwendea, akamwambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu: Panga mambo yako sawasawa katika nyumba yako kwa kuwa utakufa, hutapona.” Hezekia akageukia upande wa ukuta na kumwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi ukumbuke jinsi nilivyokutumikia kwa uaminifu na kwa moyo wangu wote, na kutenda yaliyo sawa mbele yako.” Hezekia akalia kwa uchungu sana. Kisha neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Isaya: “Nenda ukamwambie Hezekia, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yako Daudi, anasema hivi: Nimesikia ombi lako na nimeyaona machozi yako. Basi, nakuongezea miaka kumi na mitano ya kuishi. Nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mikononi mwa mfalme wa Ashuru na kuulinda.” *** *** *** *** *** *** *** *** *** *** *** *** *** *** Basi, Isaya akasema, “Chukueni andazi la tini mkaliweke kwenye jipu lake, apate kupona.” Hezekia akauliza, “Ni ishara gani itakayonijulisha kwamba mimi nitakwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu?” Isaya akamjibu, “Hii itakuwa ishara kwako kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwamba Mwenyezi-Mungu atafanya kama alivyoahidi. Nitafanya kivuli kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi, kirudi nyuma hatua kumi.” Nacho kivuli kikarudi nyuma hatua kumi. Kisha mfalme Hezekia alipopona, akatunga wimbo huu wa shukrani: “Nilisema: Nikiwa mbichi kabisa, inanibidi niage dunia. Mimi nimepangiwa kwenda kuzimu siku zote zilizonibakia. Nilisema sitamwona tena Mwenyezi-Mungu, katika nchi ya walio hai; wala sitamwona mtu yeyote tena, miongoni mwa wakazi wa ulimwengu. Makao yangu yamengolewa kwangu, kama hema la mchungaji; kama, mfumanguo nimefungasha maisha yangu; Mungu amenikatilia mbali; kabla hata mwisho wa siku amenikomesha. Usiku kucha nililia kuomba msaada; kama simba, anavunjavunja mifupa yangu; mchana na usiku ananikomesha. “Ninalia kama mbayuwayu, nasononeka kama njiwa. Macho yangu yamefifia kwa kuangalia juu. Ee Bwana, nateseka; uwe wewe usalama wangu! Lakini niseme nini: Yeye mwenyewe aliniambia, naye mwenyewe ametenda hayo. Usingizi wangu wote umenitoroka kwa sababu ya uchungu moyoni mwangu. “Ee Bwana, Sisi twaishi kutokana na yote uliyotenda, kwa hayo yote mimi binafsi pia ninaishi. Nirudishie afya, uniwezeshe kuishi. Nilipata mateso makali kwa faida yangu; lakini umeyaokoa maisha yangu kutoka shimo la uharibifu, maana umezitupa dhambi zangu nyuma yako. Huko kuzimu mtu hawezi kukushukuru wewe; waliokufa hawawezi kukushukuru wewe. Wala washukao huko shimoni hawawezi tena kutumainia uaminifu wako. Walio hai ndio wanaokushukuru, kama na mimi ninavyofanya leo. Kina baba huwajulisha watoto wao uaminifu wako. “Mwenyezi-Mungu ataniokoa. Nasi tutamsifu kwa nyimbo za vinubi siku zote za maisha yetu, nyumbani kwake Mwenyezi-Mungu.” Wakati huo, mfalme Merodak-baladani mwana wa Baladani, mfalme wa Babuloni, aliposikia kwamba Hezekia alikuwa ameugua na sasa amepona, alimtumia ujumbe pamoja na zawadi. Basi, Hezekia aliwakaribisha na kuwaonesha nyumba ya hazina: Fedha, dhahabu, viungo vya kukolezea chakula, mafuta ya thamani, vifaa vyake vyote vya kijeshi na vitu vyote vilivyokuwamo katika bohari zake. Hakuna chochote katika ikulu yake au katika nchi yake ambacho hakuwaonesha. Ndipo nabii Isaya alipokwenda kwa mfalme Hezekia na kumwuliza, “Watu hawa wamesema nini? Na, wamekujia kutoka wapi?” Naye Hezekia akamjibu “Wamenijia kutoka nchi ya mbali, huko Babuloni.” Halafu Isaya akamwuliza, “Wameona nini katika ikulu yako?” Hezekia akamjibu, “Wameona yote yaliyomo katika ikulu yangu. Hakuna chochote katika bohari zangu ambacho sikuwaonesha.” Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi: Tazama, siku zinakuja ambapo vyote vilivyomo nyumbani mwako na vitu vyote walivyokusanya wazee wako hadi leo, vitapelekwa mpaka Babuloni. Hakuna kitu chochote kitakachobaki; ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu. Tena baadhi ya watoto wako mwenyewe wa kiume watapelekwa mateka nao watakuwa matowashi katika ikulu ya mfalme wa Babuloni.” Naye Hezekia akamwambia Isaya, “Neno la Mwenyezi-Mungu ulilosema ni sawa.” Alisema hivyo kwani alifikiri, “Kutakuwa na amani na usalama muda wote niishipo.” Mungu wenu asema: “Wafarijini watu wangu, nendeni mkawafariji. Semeni na wenyeji wa Yerusalemu kwa upole, waambieni kwamba utumwa wao umekwisha, wamesamehewa uovu wao. Mwenyezi-Mungu amewaadhibu maradufu kwa sababu ya dhambi zao zote.” Sauti ya mtu anaita jangwani: “Mtayarishieni Mwenyezi-Mungu njia, nyosheni barabara kuu kwa ajili ya Mungu wetu. Kila bonde litasawazishwa, kila mlima na kilima vitashushwa; ardhi isiyo sawa itafanywa sawa, mahali pa kuparuza patalainishwa. Kisha utukufu wa Mwenyezi-Mungu utafunuliwa, na watu wote pamoja watauona. Mwenyezi-Mungu mwenyewe ametamka hayo.” Sikiliza! Kuna sauti inasema, “Tangaza!” Nami nikauliza, “Nitangaze nini?” Naye: “Tangaza: Binadamu wote ni kama majani; uthabiti wao ni kama ua la shambani. Majani hunyauka na ua hufifia, Mwenyezi-Mungu avumishapo upepo juu yake. Hakika binadamu ni kama majani. Majani hunyauka na ua hufifia, lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.” Nenda juu ya mlima mrefu, ewe Siyoni, ukatangaze habari njema. Paza sauti yako kwa nguvu, ewe Yerusalemu, ukatangaze habari njema. paza sauti yako bila kuogopa. Iambie miji ya Yuda: “Mungu wenu anakuja.” Bwana Mungu anakuja na nguvu, kwa mkono wake anatawala. Zawadi yake iko pamoja naye, na tuzo lake analo. Atalilisha kundi lake kama mchungaji, atawakusanya wanakondoo mikononi mwake, atawabeba kifuani pake, na kondoo wanyonyeshao atawaongoza polepole. Nani awezaye kupima maji ya bahari kwa konzi yake, kuzipima mbingu kwa mikono yake? Nani awezaye kuutia udongo wa dunia kikombeni; kuipima milima kwa mizani au vilima kwa kipimo cha uzani? Nani awezaye kuiongoza akili ya Mwenyezi-Mungu, au kuwa mshauri wake na kumfunza? Mwenyezi-Mungu alimtaka nani shauri, ndipo akapata kuwa mwenye ujuzi? Nani aliyemfunza njia za haki? Nani aliyemfundisha maarifa, na kumwonesha namna ya kuwa na akili? Kwake mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, ni kama vumbi juu ya mizani. Kwake visiwa ni vyepesi kama vumbi laini. Kuni zote za Lebanoni na wanyama wake wote havitoshi kwa sadaka ya kuteketezwa mbele yake. Mataifa yote si kitu mbele yake; kwake ni vitu duni kabisa na batili. Mtamlinganisha Mungu na nini basi, au ni kitu gani cha kumfananisha naye? Je, anafanana na kinyago? Hicho, fundi hukichonga, mfua dhahabu akakipaka dhahabu, na kukitengenezea minyororo ya fedha! Au ni sanamu ya mti mgumu? Hiyo ni ukuni mtu anaochagua, akamtafuta fundi stadi, naye akamchongea sanamu imara! Je, nyinyi bado hamjui? Je, hamjapata kusikia? Je, hamkuambiwa tangu mwanzo? Je, hamjafahamu mwanzo wa dunia? Dunia iliumbwa na huyo aketiye juu ya mbingu; kutoka huko wakazi wa dunia ni kama panzi! Yeye amezitandaza mbingu kama pazia, na kuzikunjua kama hema la kuishi. Yeye huwaporomosha wakuu wenye nguvu, watawala wa dunia huwafanya kuwa si kitu. Mara tu wanaposimikwa na kuanza kuota, hata kabla hawajatoa mizizi kama miti udongoni, Mwenyezi-Mungu akiwapulizia hunyauka, kimbunga huwapeperusha kama makapi! Mungu Mtakatifu auliza hivi: “Nani basi, mtakayemlinganisha nami? Je, kuna mtu aliye kama mimi?” Inueni macho yenu juu mbinguni! Je, ni nani aliyeziumba nyota hizo? Ni yule aziongozaye kama jeshi lake, anayeijua idadi yake yote, aziitaye kila moja kwa jina lake. Kwa sababu yeye ni mwenye nguvu nyingi, hakuna hata moja inayokosekana. Enyi watu wa Israeli wazawa wa Yakobo, kwa nini mnalalamika na kusema: “Mwenyezi-Mungu hatujali sisi! Mungu wetu hajali haki yetu!” Je, nyinyi bado hamjui? Je, hamjapata kusikia? Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu wa milele; yeye ndiye Muumba wa kila kitu duniani. Yeye hafifii kamwe wala kuishiwa nguvu. Maarifa yake hayachunguziki. Yeye huwapa uwezo walio hafifu, wanyonge huwapa nguvu. Hata vijana watafifia na kulegea; naam, wataanguka kwa uchovu. Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu, watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea bila kulegea. Mungu asema hivi: “Enyi wakazi wa mbali nyamazeni mnisikilize! Enyi mataifa jipeni nguvu; jitokezeni mkatoe hoja zenu, na tuje pamoja kwa hukumu. “Nani, ila mimi, aliyemwita shujaa toka mashariki, mtu ambaye hupata ushindi popote aendako? Mimi huyatia mataifa makuchani mwake, naye huwaponda wafalme chini ya miguu yake! Upanga wake huwafanya kuwa kama vumbi, kwa upinde wake huwapeperusha kama makapi. Yeye huwafuatia na kupita salama; huenda kasi kana kwamba hagusi chini. Nani aliyefanya yote haya yatendeke? Ni nani aliyepanga wakati wa kila tukio? Mimi Mwenyezi-Mungu nipo tangu mwanzo, mimi nitakuwapo hata milele. “Wakazi wa mbali wameona niliyotenda, wakaogopa; dunia yote inatetemeka kwa hofu. Watu wote wamekusanyika, wakaja. Kila mmoja anamhimiza mwenzake akisema, ‘Haya! Jipe moyo!’ Fundi anamhimiza mfua dhahabu, naye alainishaye sanamu kwa nyundo, anamhimiza anayeiunga kwa misumari. Wote wanasema, ‘Imeungika vizuri sana!’ Kisha wanaifunga kwa misumari isitikisike. “Sikiliza ewe Israeli, mtumishi wangu, wewe, Yakobo ambaye nimekuchagua, wewe mzawa wa Abrahamu, rafiki yangu; wewe niliyekuleta toka miisho ya dunia, wewe niliyekuambia: ‘Wewe u mtumishi wangu; mimi sikukutupa, bali nilikuchagua.’ Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi. “Naam! Wote waliokuwakia hasira, wataaibishwa na kupata fedheha. Wote wanaopingana nawe, watakuwa si kitu na kuangamia. Utawatafuta hao wanaopingana nawe, lakini watakuwa wameangamia. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ndimi ninayetegemeza mkono wako. Mimi ndimi ninayekuambia: ‘Usiogope, nitakusaidia.’” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wa Yakobo dhaifu kama mdudu, enyi Waisraeli, msiogope! Mimi Mwenyezi-Mungu nasema nitawasaidia. Mimi ni Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli. Nitawafanya muwe kama chombo cha kupuria, chenye meno mapya na makali. Mtaipura milima na kuipondaponda; vilima mtavisagasaga kama makapi. Mtaipepeta milima hiyo, nao upepo utaipeperushia mbali, naam, dhoruba itaitawanya huko na huko. Nanyi mtafurahi kwa sababu yangu Mwenyezi-Mungu; mtaona fahari kwa sababu yangu Mungu Mtakatifu wa Israeli. “Maskini na fukara wakitafuta maji wasipate, wakiwa wamekauka koo kwa kiu, mimi Mwenyezi-Mungu nitawajibu; mimi Mungu wa Israeli, sitawaacha. Nitabubujisha mito kwenye milima mikavu, na chemchemi katika mabonde. Nitaigeuza nyika kuwa bwawa la maji, na nchi kame kuwa chemchemi za maji. Nitapanda miti huko nyikani: Mierezi, mikakaya, mijohoro, na mizeituni; nitaweka huko jangwani: Miberoshi, mivinje na misonobari. Watu wataona jambo hilo, nao watatambua na kuelewa kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nimetenda hayo, mimi Mtakatifu wa Israeli nimefanya jambo hilo.” Mwenyezi-Mungu, Mfalme wa Yakobo, asema: “Enyi miungu ya mataifa, njoni mtoe hoja zenu! Leteni hoja zenu, mtuambie yatakayotukia. Tuambieni matukio ya kwanza yalikuwa yapi nasi tutayatafakari moyoni. Au tutangazieni yajayo, tujue yatakayokuja. Tuambieni yatakayotokea baadaye, nasi tujue basi kama nyinyi ni miungu. Fanyeni kitu chochote, chema au kibaya, ili tutishike na kuogopa. Hakika, nyinyi si kitu kabisa. hamwezi kufanya chochote kile. Anayechagua kuwaabudu nyinyi ni chukizo. “Nimechochea mtu toka kaskazini, naye amekuja; naam, nimemchagua mtu toka mashariki, naye atalitamka jina langu. Yeye atawakanyaga wafalme kama tope, kama vile mfinyanzi apondavyo udongo wake. Nani aliyebashiri haya tangu mwanzo, hata sisi tupate kuyatambua? Nani aliyetangulia kuyatangaza, ili sasa tuseme, alisema ukweli? Hakuna hata mmoja wenu aliyeyataja, wala hakuna aliyesikia maneno yenu. Mimi ni yule wa kwanza, niliyetangaza kwa Siyoni, nikapeleka Yerusalemu mjumbe wa habari njema. Nimeangalia kwa makini sana, lakini simwoni yeyote yule; hamna yeyote kati ya hao miungu awezaye kushauri; nikiuliza hakuna awezaye kunijibu. La! Miungu hiyo yote ni udanganyifu, haiwezi kufanya chochote; sanamu zao za kusubu ni upuuzi. “Tazameni mtumishi wangu ninayemtegemeza; mteule wangu ambaye moyo wangu umependezwa naye. Nimeiweka roho yangu juu yake, naye atayaletea mataifa haki. Hatalia wala hatapiga kelele, wala hatapaza sauti yake barabarani. Mwanzi uliochubuka hatauvunja, utambi ufukao moshi hatauzima; ataleta haki kwa uaminifu. Yeye hatafifia wala kufa moyo, hata atakapoimarisha haki duniani. Watu wa mbali wanangojea mwongozo wake.” Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu aliyeziumba mbingu, akazitandaza kama hema, yeye aliyeiunda nchi na vyote vilivyomo, yeye awapaye watu waliomo pumzi, na kuwajalia uhai wote waishio humo: “Mimi Mwenyezi-Mungu nimekuita kutenda haki, nimekushika mkono na kukulinda. Kwa njia yako nitaweka ahadi na watu wote, wewe utakuwa mwanga wa mataifa. Utayafumbua macho ya vipofu, utawatoa wafungwa gerezani, waliokaa gizani utawaletea uhuru. Jina langu mimi ni Mwenyezi-Mungu; utukufu wangu sitampa mwingine, wala sifa zangu sanamu za miungu. Tazama, mambo niliyotabiri yametukia; na sasa natangaza mambo mapya, nakueleza hayo kabla hayajatukia.” Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya! Dunia yote iimbe sifa zake: Bahari na vyote vilivyomo, nchi za mbali na wakazi wake; jangwa na miji yake yote ipaaze sauti, vijiji vya wakazi wa Kedari vimsifu, wakazi wa Sela waimbe kwa shangwe; wapaaze sauti kutoka mlimani juu. Wote wakaao nchi za mbali, na wamtukuze na kumsifu Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu ajitokeza kama shujaa; kama askari vitani ajikakamua kupigana. Anapaza sauti kubwa ya vita, na kujionesha mwenye nguvu dhidi ya maadui zake. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kwa muda mrefu sasa nimenyamaza, nimekaa kimya na kujizuia; lakini sasa nitalia kama mama anayejifungua, anayetweta pamoja na kuhema. Nitaharibu milima na vilima, na majani yote nitayakausha. Mito ya maji nitaigeuza kuwa nchi kavu, na mabwawa ya maji nitayakausha. “Nitawaongoza vipofu katika njia wasiyoifahamu, nitawaongoza katika njia ambazo hawazijui. Mbele yao giza nitaligeuza kuwa mwanga, na mahali pa kuparuza patakuwa laini. Huo ndio mpango wangu wa kufanya, nami nitautekeleza. Wote wanaotegemea sanamu za miungu, wote wanaoziambia: Nyinyi ni miungu yetu; watakomeshwa na kuaibishwa. “Sikilizeni enyi viziwi! Tazameni enyi vipofu, mpate kuona! Nani aliye kipofu ila mtumishi wangu? Nani aliye kiziwi kama mjumbe ninayemtuma? Ni nani aliye kipofu kama huyu niliyemweka wakfu, au kipofu kama mtumishi wa Mwenyezi-Mungu? Nyinyi mmeona mambo mengi, lakini hamwelewi kitu. Masikio yenu yako wazi, lakini hamsikii kitu!” Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya uaminifu wake, alipenda kukuza mwongozo wake na kuutukuza. Lakini hawa ni watu walioibiwa mali na kuporwa! Wote wamenaswa mashimoni, wamefungwa gerezani. Wamekuwa kama mawindo bila mtu wa kuwaokoa, wamekuwa nyara na hakuna asemaye, “Waokolewe!” Je, mtatega sikio kusikia kitu hiki? Nani kati yenu atakayesikiliza vizuri yatakayotukia? Ni nani aliyewatia Waisraeli mikononi mwa adui zao? Nani aliyewaacha wanyanganywe mali zao? Ni Mwenyezi-Mungu ambaye tumemkosea! Wazee wetu walikataa kuzifuata njia zake, wala hawakuzitii amri zake. Kwa hiyo aliwamwagia hasira yake kali, akawaacha wakumbane na vita vikali. Hasira yake iliwawakia kila upande, lakini wao hawakuelewa chochote; iliwachoma, lakini hawakutilia jambo hilo maanani. Mwenyezi-Mungu aliyewaumba enyi watu wa Yakobo, yeye aliyewafanya enyi watu wa Israeli, asema: “Msiogope, maana mimi nimewakomboa; nimewaita kwa jina nanyi ni wangu. Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza. Maana mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, Mungu Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wenu. Nitaitoa nchi ya Misri iwe fidia yenu, nitaitoa Kushi na Seba ili mwachwe huru. Kwa vile mna thamani mbele yangu, kwa kuwa nimewapa hadhi na kuwapenda, mimi nawaacha watu kusudi niwapate nyinyi, nayaachilia mataifa badala ya maisha yenu. Msiogope maana mimi nipo pamoja nanyi. “Nitawarudisha wazawa wenu toka mashariki, nitawakusanyeni kutoka magharibi. Nitaiambia kaskazini, ‘Waache waondoke’, na kusini, ‘Usiwazuie’! Warudisheni watu kutoka mbali, kutoka kila mahali duniani. Kila mmoja hujulikana kwa jina langu, niliwaumba wote na kuwafanya kwa ajili ya utukufu wangu.” Waleteni mbele watu hao, ambao wana macho lakini hawaoni wana masikio lakini hawasikii! Mataifa yote na yakusanyike, watu wote na wakutane pamoja. Nani kati ya miungu yao awezaye kutangaza yatakayotukia? Nani awezaye kutuonesha yanayotukia sasa? Wawalete mashahidi wao kuthibitisha kwamba walifanya hivyo. Waache wasikilize na kusema, “Ilikuwa kweli.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi Waisraeli ni mashahidi wangu; niliwachagua muwe watumishi wangu, mpate kunijua na kuniamini, kwamba ndimi peke yangu Mungu. Kabla yangu hajapata kuwapo mungu mwingine, wala hatakuwapo mungu mwingine. “Mimi peke yangu ndimi Mwenyezi-Mungu, hakuna mkombozi mwingine ila mimi. Nilitangaza yale ambayo yangetukia, kisha nikaja na kuwakomboa. Hakuna mungu mwingine aliyewahi kufanya hivyo, nanyi ni mashahidi wangu. Mimi ni Mungu na nitakuwa Mungu daima. Hakuna awezaye kuiepa nguvu yangu; hakuna awezaye kupinga ninayofanya.” Mwenyezi-Mungu, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi: “Kwa ajili yenu nitatuma jeshi Babuloni. Nitayavunjilia mbali malango ya mji wake, na kelele za hao Wakaldayo zitageuka maombolezo. Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wenu; Mimi ndimi Muumba wa Israeli, Mfalme wenu.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wakati mmoja nilifanya barabara baharini nikaweka njia kati ya mawimbi makubwa. Nililipiga jeshi lenye nguvu, jeshi la magari na farasi wa vita, askari na mashujaa wa vita. Niliwaangusha chini wasiweze kuinuka tena, niliwakomesha na kuwazima kama utambi wa taa. Sasa nasema: ‘Msiyanganganie mambo yaliyopita, wala msifikirie vitu vya zamani. Tazameni, mimi ninafanya kitu kipya. Kinafanyika sasa hivi, nanyi mtaweza kukiona. Nitafanya njia nyikani, na kububujisha mito jangwani. Wanyama wa porini wataniheshimu, kina mbweha na kina mbuni, maana nitaweka maji nyikani, na kububujisha mito jangwani, ili kuwanywesha watu wangu wateule, watu niliowaumba kwa ajili yangu mwenyewe, ili wazitangaze sifa zangu!’ “Lakini ewe taifa la Yakobo, hukuniabudu mimi; enyi watu wa Israeli, mlinichoka mimi! Hamjaniletea kondoo wenu wa sadaka za kuteketezwa, wala kuniheshimu kwa tambiko zenu. Nami sikuwalemeza kwa kutaka sadaka, wala sikuwachosha kwa kuwadai ubani. Hamkuninunulia manukato kwa faida yenu, wala kuniridhisha kwa nyama nono za tambiko. Badala yake dhambi zenu zimekuwa mzigo kwangu, mmenichosha kabisa kwa makosa yenu. Walakini mimi ndimi niliyefuta makosa yenu kwa heshima yangu, ndimi niyafutaye makosa kwa ajili yangu mwenyewe, na wala sitazikumbuka dhambi zenu. “Niambie kama mna kisa nami, njoo tukahojiane; toeni mashtaka yenu ili tuuone ukweli wenu! Babu yenu wa kwanza alitenda dhambi, wapatanishi wenu waliniasi. Kwa hiyo niliwafanya haramu wakuu wa mahali patakatifu nikawaacha watu wa Yakobo waangamizwe, naam, nikawaacha Waisraeli watukanwe.” “Sikiliza ewe taifa Israeli mtumishi wangu; sikiliza ewe kizazi cha Yakobo mteule wangu. Mimi, Mwenyezi-Mungu Muumba wako, niliyekufanya tangu tumboni mwa mama yako, nimekuja kukusaidia wewe. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema: Usiogope, ewe taifa la Yakobo, mtumishi wangu, naam, usiogope ewe Yeshuruni mteule wangu. “Nitaimwagilia maji nchi iliyokauka, na kutiririsha mto katika nchi kame. Nitawamiminia roho yangu wazawa wako, nitawamwagia watoto wako baraka yangu. Watachipua kama nyasi penye maji mengi, kama majani kandokando ya vijito. “Mmoja atasema: ‘Mimi ni wa Mwenyezi-Mungu’, mwingine atajiita kwa jina la Yakobo, mwingine ataandika mkononi mwake, ‘Wa Mwenyezi-Mungu’, na kujitambulisha kwa jina la Israeli.” Mwenyezi-Mungu, Mfalme na Mkombozi wa Israeli, naam, Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Mimi ni wa kwanza na wa mwisho; hakuna Mungu mwingine ila mimi. Ni nani Mungu aliye kama mimi? Mwache atangaze na kusema wazi mbele yangu. Nani alitangaza hapo kale mambo ambayo yatatukia? Na watuambie yale ambayo bado kutokea. Enyi watu wangu, msiogope wala msiwe na hofu, Je, sikuwaambia tangu zamani mambo yatakayotokea? Nyinyi ni mashahidi wangu. Je, yuko Mungu mwingine ila mimi? Je, kuna mwenye nguvu mwingine? Huyo simjui!” Watu wote wanaotengeneza sanamu za miungu ni bure kabisa; na vitu hivyo wanavyovifurahia haviwafai chochote. Wanaoshuhudia hiyo miungu ya uongo ni vipofu na wajinga. Kwa hiyo hao wataaibishwa! Ajabu ya mtu kutengeneza sanamu au kinyago cha mungu ambaye hawezi kumsaidia chochote! Hakika wote wanaomheshimu wataaibishwa, tena hao mafundi wa sanamu ni binadamu tu. Basi, wakutane wote, wajitokeze, nao watatishika na kuaibishwa. Mfuachuma huchukua madini, akayayeyusha motoni na kufua sanamu. Huigongagonga kwa nyundo ili kuipa umbo kwa mikono yake yenye nguvu. Wakati wote huo yeye huona njaa na kuchoka; huona kiu na nguvu kumwishia. Kadhalika naye seremala hupima kipande cha mbao, akakitia alama kwa kalamu yake, kisha kwa vifaa vyake hukichonga na kukipa umbo la binadamu na sura ya kupendeza; kisha akaiweka sanamu hiyo ya mungu mahali pake pa pekee. Mtu hukata mti wa mwerezi ili autumie, au huchagua mberoshi au mwaloni. Huuacha ukue kati ya miti ya msituni. Au hupanda mwerezi na mvua huustawisha. Sehemu ya mti huo itatumiwa kama kuni; mtu huota moto wake na kuoka mikate yake juu yake. Sehemu nyingine ya mti huohuo, mtu hujichongea sanamu ya mungu, akainakshi, halafu akaiabudu. Kisha huchukua kuni zake akaoka nazo moto, akachoma nyama juu yake, akala, akashiba. Halafu hukaa hapo akiota moto na kusema, “Naam! Ama kweli nimepata joto! Huo ndio moto!” Sehemu iliyobaki ya mti huohuo, hujichongea sanamu ya mungu, kinyago chake, kisha huisujudia na kuiabudu. Huiomba akisema, “Wewe ni mungu wangu, niokoe!” Watu hao hawajui wala hawaelewi kitu chochote. Wamefumbwa macho wasiweze kuona; kadhalika na akili zao wasiweze kufahamu. Hakuna awezaye kutafakari; au kuwa na akili na kufikiri na kusema: “Nusu ya mti huo niliwashia moto; tena nikaoka mikate juu ya makaa yake, nikachoma nyama, nikala. Je, sehemu iliyobaki nitatengeneza sanamu ambayo ni chukizo na kukisujudia hicho kipande cha mti?” La! Fikira zake zimeambatana na hicho ambacho ni majivu tu! Mtu huyo amepotoka hata hawezi kujiokoa mwenyewe na kusema: “Kweli ninachoshika mkononi ni udanganyifu mtupu!” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ewe taifa la Yakobo kumbuka; naam, kumbuka ewe Israeli: Wewe ni mtumishi wangu. Nilikuumba ili uwe mtumishi wangu, nami kamwe sitakusahau. Nimeyafagilia mbali makosa yako kama wingu, nimezifanya dhambi zako zitoweke kama ukungu. Rudi kwangu maana mimi nimekukomboa.” Imbeni kwa furaha enyi mbingu, kwa sababu ya hayo aliyotenda Mwenyezi-Mungu. Pazeni sauti enyi vilindi vya dunia! Imbeni kwa furaha enyi milima! Enyi misitu na miti yote iliyomo, imbeni. Maana Mwenyezi-Mungu amewakomboa wazawa wa Yakobo, naye atatukuka katika nchi ya Israeli. Mwenyezi-Mungu, Mkombozi wako, aliyekuumba tangu tumboni mwa mama yako, asema: “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu niliyeumba vitu vyote. Mimi peke yangu nilizitandaza mbingu, niliiumba dunia kwa nguvu yangu mwenyewe! Mimi huzivuruga ishara za watabiri waongo na kuwapumbaza waaguzi. Mimi huyakanusha maneno ya wenye hekima na kufanya ujuzi wao kuwa upumbavu. Lakini huuthibitisha ujumbe wa mtumishi wangu, na kukamilisha maaguzi ya wajumbe wangu. Mimi ndimi niuambiaye mji wa Yerusalemu: Wewe Yerusalemu, utakaliwa tena na watu. Na miji ya Yuda: Nyinyi mtajengeka tena: Magofu yenu nitayarekebisha tena. Mimi ndimi ninayeviamuru vilindi: Kaukeni. Ndimi nimwambiaye Koreshi: Wewe utawachunga watu kwa niaba yangu. Wewe utatekeleza mipango yangu yote. Ndimi ninayesema kuhusu Yerusalemu: Wewe Yerusalemu utajengwa tena upya; na juu ya hekalu: Msingi wako utawekwa tena.” Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Koreshi: “Wewe ni mfalme wangu niliyekuteua; mimi naitegemeza nguvu yako ili uyashinde mataifa mbele yako, na kuzivunja nguvu za wafalme. Mimi nayafungua malango ya mji mbele yako, na hakuna lango litakalofungwa. Mimi nitakutangulia, na kuisawazisha milima mbele yako. Nitaivunjavunja milango ya shaba, na kuvikatakata vizuizi vyake vya chuma. Nitakupa hazina zilizofichwa gizani, na mali iliyo mahali pa siri, upate kutambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninayekuita kwa jina lako. Kwa ajili ya mtumishi wangu Yakobo, naam, kwa ajili ya mteule wangu Israeli, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la heshima ingawa wewe hunijui. “Mimi ni Mwenyezi-Mungu, wala hakuna mwingine; hakuna Mungu mwingine ila mimi. Ninakuimarisha ingawa wewe hunijui, ili watu wote, toka mashariki hadi magharibi, wajue kwamba hakuna Mungu mwingine ila mimi; mimi ni Mwenyezi-Mungu na hakuna mwingine. Mimi hufanya mwanga na kuumba giza; huleta fanaka na kusababisha balaa. Mimi Mwenyezi-Mungu hutenda vitu hivi vyote. Enyi mbingu, nyesheni kutoka huko juu, mawingu na yadondoshe uadilifu; dunia na ifunuke, ichipushe wokovu, na kuchanusha uadilifu pia! Mimi, Mwenyezi-Mungu nimefanya hayo.” Ole wake mtu ashindanaye na Muumba wake, mtu aliye chombo cha udongo kushindana na mfinyanzi wake! Je, udongo humwuliza anayeufinyanga: “Unatengeneza nini hapa?” Au kumwambia, “Kazi yako si kamili!” Ole wake mtoto amwambiaye baba yake, “Kwa nini umenizaa?” Au amwambiaye mama yake, “Ya nini umenileta duniani?” Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli, Mungu, Muumba wa Israeli asema: “Je, mwathubutu kuniuliza juu ya watoto wangu, au kuniamuru juu ya kazi zangu mwenyewe? Ni mimi niliyeifanya dunia, na kuumba binadamu aishiye humo. Mikono yangu ndiyo iliyozitandaza mbingu, na jeshi lote la nyota liko kwa amri yangu. Ni mimi niliyemwamuru Koreshi kuchukua hatua, atekeleze matakwa yangu. Nitazifanikisha njia zake zote; ataujenga upya mji wangu Yerusalemu, na kuwapa uhuru watu wangu walio uhamishoni, bila kutaka malipo wala zawadi.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amesema. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Utajiri wa Misri na bidhaa za Kushi, pamoja na za watu wa Seba, majitu marefu, zitakuja kwako mwenyewe wewe taifa la Israeli, zote zitakuwa mali yako. Watu hao watakutumikia wamefungwa minyororo; watakusujudia na kukiri wakisema: ‘Kwako kuna Mungu wa kweli, wala hakuna Mungu mwingine ila yeye.’” Kweli wewe ni Mungu uliyefichika, Mungu wa Israeli, Mungu Mwokozi. Watengenezaji sanamu wataaibika na kufadhaika, wote kwa pamoja watavurugika. Lakini taifa la Israeli litaokolewa na Mwenyezi-Mungu, litapata wokovu wa milele. Halitaaibishwa wala kufadhaishwa milele. Mwenyezi-Mungu, Mungu pekee, ndiye aliyeiumba dunia, ndiye aliyeiumba na kuitegemeza. Hakuiumba iwe ghasia na tupu, ila aliiumba ikaliwe na viumbe vyake. Yeye asema sasa: “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, wala hakuna mwingine. Mimi sikunena kwa siri, wala katika nchi yenye giza. Mimi sikuwaambia wazawa wa Yakobo wanitafute katika ghasia. Mimi Mwenyezi-Mungu husema ukweli, maneno yangu ni ya kuaminika.” Enyi watu wa mataifa mliosalia, kusanyikeni pamoja mje! Nyinyi mmekosa akili: Nyinyi mwabeba sanamu za miti na kumwomba mungu asiyeweza kuokoa watu. Semeni wazi na kutoa hoja zenu; shaurianeni pamoja! Ni nani aliyetangaza zamani matukio ya sasa? Ni nani aliyetamka mambo haya zamani? Je, haikuwa mimi Mwenyezi-Mungu? Hakuna Mungu mwingine ila mimi! Mimi ni Mungu wa haki na mwokozi; hakuna mwingine ila mimi. Nigeukieni mimi mpate kuokolewa, popote mlipo duniani. Maana mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine. Mimi nimeapa kwa nafsi yangu, ninachotamka ni ukweli, neno langu halitarudi nyuma: Kila binadamu atanipigia magoti, kila mtu ataapa uaminifu. “Watasema juu yangu, ‘Haki na nguvu viko kwa Mwenyezi-Mungu peke yake.’” Wote waliomwakia hasira Mwenyezi-Mungu watamjia yeye na kuaibishwa. Lakini wazawa wa Israeli watapata ushindi kwake Mwenyezi-Mungu na kufurahi. “Wewe Beli umeanguka; Nebo umeporomoka. Wakati mmoja watu walibeba sanamu zenu. Sasa wanazibeba mgongoni mwa wanyama, hao wanyama wachovu wamelemewa. Nyinyi mmeanguka na kuvunjika, hamwezi kuviokoa vinyago vyenu; nyinyi wenyewe pia mtapelekwa uhamishoni! “Sikilizeni enyi wazawa wa Yakobo, nisikilizeni enyi mabaki ya watu wangu wa Israeli. Mimi niliwatunzeni tangu mlipozaliwa; niliwabebeni tangu tumboni mwa mama yenu. Mimi ni yuleyule hata katika uzee wenu; hata katika uzee wenu mimi nitawabeba. Nilifanya hivyo kwanza, nitafanya hivyo tena. Nitawabeba nyinyi na kuwaokoa. “Mtanifananisha na nani, tufanane? Je, mwaweza kunilinganisha na nani, tulingane? Watu humimina dhahabu kutoka mifuko yao, hupima fedha kwenye mizani zao, wakamwajiri mfua dhahabu atengeneze sanamu kisha huisujudu na kuiabudu! Hujitwisha sanamu hiyo mabegani, wakaibeba, kisha huiweka mahali pake, ikakaa papo hapo; kamwe haiwezi hata kusogea kutoka hapo ilipo. Mtu akiililia, haiwezi kumwitikia, wala haiwezi kumwokoa mtu katika taabu zake. “Kumbukeni jambo hili na kutafakari, liwazeni akilini mwenu enyi wakosefu. Kumbukeni mambo niliyotenda hapo kale! Mimi ndimi Mungu na hakuna mwingine; naam, mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine kama mimi. Nilitangaza mambo ya mwisho tangu mwanzo, tangu kale nilitangaza mambo yatakayotukia. Lengo langu litatimia; mimi nitatekeleza nia yangu yote. Ninamwita tai wangu kutoka mashariki, naam, msiri wangu kutoka nchi ya mbali. Mimi nimenena na nitayafanya; mimi nimepanga nami nitatekeleza. “Nisikilizeni, enyi wenye vichwa vigumu, nisikilizeni enyi mlio mbali na ukombozi. Siku ya kuwakomboa naileta karibu, haiko mbali tena; siku ya kuwaokoeni haitachelewa. Nitauokoa mji wa Siyoni, kwa ajili ya Israeli, fahari yangu. “Teremka uketi mavumbini ewe Babuloni binti mzuri! Keti chini pasipo kiti cha enzi ewe binti wa Wakaldayo! Tokea sasa hutaitwa tena mwororo wala nadhifu. Twaa mawe ya kusagia, usage unga kama mtumwa! Vua utaji wako, ukavue na mavazi yako! Pandishia vazi lako miguuni, ukavuke mito. Watu watauona uchi wako; naam, wataiona aibu yako. Mimi nitalipiza kisasi, wala sitamhurumia yeyote.” Mkombozi wetu ndiye Mtakatifu wa Israeli; Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndilo jina lake. Mwenyezi-Mungu asema: “Ewe taifa la Wakaldayo lililo kama binti mzuri, keti kimya na kutokomea gizani. Maana umepoteza hadhi yako ya kuwa bimkubwa wa falme. Niliwakasirikia watu wangu Israeli, nikawafanya watu wangu kuwa haramu. Niliwatia mikononi mwako, nawe hukuwaonea huruma; na wazee uliwatwisha nira nzito mno. Ulijisemea moyoni: ‘Nitakuwa malkia milele’, nawe hukuyatafakari mambo yanayotokea, wala kufikiri mwisho wake. “Sasa, basi, sikiliza ewe mpenda anasa, wewe unayedhani kuwa u salama, na kujisemea: ‘Ni mimi tu, na hakuna mwingine isipokuwa mimi. Kamwe sitakuwa mjane, wala sitafiwa na wanangu.’ Haya yote mawili yatakupata, ghafla, katika siku moja: Kupoteza watoto wako na kuwa mjane, ijapokuwa una wingi wa uchawi wako, na nguvu nyingi za uganga wako. “Ulijiona salama katika uovu wako; ukajisemea, ‘Hakuna mtu anayeniona.’ Hekima na elimu yako vilikupotosha, ukajisemea moyoni mwako, ‘Mimi ndiye; hakuna mwingine anayenishinda.’ Lakini maafa yatakupata ambayo hutaweza kujiepusha nayo. Balaa litakukumba ambalo hutaweza kulipinga; maangamizi yatakujia ghafla ambayo hujapata kamwe kuyaona. Endelea basi na uganga wako, tegemea wingi wa uchawi wako. Wewe uliyapania hayo tangu ujana wako ukitumainia kwamba utafanikiwa au kusababisha kitisho kwa watu! Wewe umejichosha bure na washauri wako. Basi, na wajitokeze hao wanajimu wakuokoe! Wao huzigawa mbingu sehemusehemu, huzichunguza nyota na kubashiri kila mwezi yatakayokupata. “Kumbuka, wao ni kama mabua makavu: Moto utayateketezea mbali! Hawawezi hata kujiokoa wenyewe mbali na ukali wa moto huo. Moto huo si wa kujipatia joto, huo si moto wa kuota! Ndivyo watakavyokuwa hao uliowategemea hivyo, hao uliojishughulisha nao tangu ujana wako. Watatangatanga kila mmoja njia yake; hakuna hata mmoja atakayeweza kukuokoa.” Sikilizeni, enyi watu wa Yakobo, enyi mnaojulikana kwa jina la Israeli, nyinyi mlio wa ukoo wa Yuda. Nyinyi huapa kwa jina la Mwenyezi-Mungu, na kudai mnamwabudu Mungu wa Israeli; lakini hayo si ukweli wala sawa. Nyinyi mnaona fahari kujiita watu wa mji mtakatifu, na kujidai kumtegemea Mungu wa Israeli, ambaye jina lake ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi. “Nilitangaza zamani matukio ya awali, niliyatamka mimi mwenyewe na kuyafanya yajulikane kwenu. Mara nikaanza kuyatekeleza, nayo yakapata kutukia. Lakini nilikujua wewe kuwa mkaidi; kichwa kigumu kama chuma, uso wako mkavu kama shaba. Kwa hiyo nilikutangazia tangu zamani, kabla hayajatukia mimi nilikutangazia, usije ukasema, ‘Kinyago changu kiliyatenda hayo, sanamu zangu za kuchonga na kusubu ziliyafanya.’ “Wewe uliyasikia na sasa unayaona yote. Kwa nini huwezi kuyakiri? Tangu sasa nitakujulisha mambo mapya; mambo yaliyofichika ambayo hukuyajua. Mambo hayo yanatukia sasa; hukupata kuyasikia kabla ya leo, hivyo huwezi kusema, ‘Aa! Nilikwisha yajua.’ Hujapata kamwe kuyasikia wala kuyajua; tangu zamani masikio yako hayakuyasikia. Nilijua kuwa wewe ni mwenye hila, na kwamba wewe ni mwasi tangu kuzaliwa. “Kwa heshima ya jina langu, ninaiahirisha hasira yangu; kwa ajili ya heshima yangu, ninaizuia nisije nikakuangamiza. Mimi nitawajaribu lakini si kama fedha katika tanuri. Nitawajaribu katika tanuri ya taabu. Ninafanya hivyo kwa ajili yangu mwenyewe. Kwa nini jina langu lidharauliwe? Utukufu wangu siwezi kumpa mwingine! “Nisikilize ee taifa la Yakobo, nisikilize ee Israeli niliyekuita. Mimi ndiye Mungu; mimi ni wa kwanza na wa mwisho. Kwa mkono wangu niliuweka msingi wa dunia, mimi mwenyewe nilizitandaza mbingu. Nikiziita mbingu na dunia, zinasimama haraka mbele yangu. “Kusanyikeni nyote msikilize! Nani kati ya miungu yenu aliyetabiri vitu hivi? Mimi Mwenyezi-Mungu nampenda Koreshi; yeye atatekeleza lengo langu kuhusu Babuloni, naam, yeye atawashambulia Wakaldayo. Mimi, naam, mimi nimeyasema na kumwita; nimemleta, naye atafaulu katika mpango wake. Njoni karibu nami msikie jambo hili: Tangu mwanzo mimi sikusema kwa siri, tangu mambo hayo yaanze kutendeka, nimekuwapo.” Sasa, Bwana Mungu amenituma, na kunipa nguvu ya roho yake. Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli, Mkombozi wako, asema hivi: “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ninayekufundisha kwa faida yako, ninayekuongoza katika njia unayotakiwa kwenda. Laiti ungalizitii amri zangu! Hapo baraka zingekutiririkia kama mto, ungepata fanaka kwa wingi kama mawimbi ya bahari. Wazawa wako wangekuwa wengi kama mchanga, naam, wangekuwa wengi kama chembe za mchanga. Jina lao kamwe lisingaliondolewa, kumbukumbu lao halingalitoweka mbele yangu.” Sasa, ondokeni Babuloni! Kimbieni kutoka Kaldayo! Tangazeni jambo hili kwa sauti za shangwe, enezeni habari zake kila mahali duniani. Semeni: “Mwenyezi-Mungu amelikomboa taifa la mtumishi wake Yakobo.” Alipowaongoza jangwani hawakuona kiu, aliwatiririshia maji kutoka mwambani, aliupasua mwamba maji yakabubujika. Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu waovu sitawapa amani.” Nisikilizeni, enyi nchi za mbali, tegeni sikio, enyi watu wa mbali! Mwenyezi-Mungu aliniita kabla sijazaliwa, alitaja jina langu nikiwa tumboni mwa mama yangu. Aliyapa ukali maneno yangu kama upanga mkali, alinificha katika kivuli cha mkono wake; aliufanya ujumbe wangu mkali kama ncha ya mshale, akanificha katika podo lake. Aliniambia, “Wewe ni mtumishi wangu; kwako, Israeli, watu watanitukuza.” Lakini mimi nikafikiri, “Nimeshughulika bure, nimetumia nguvu zangu bure kabisa.” Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu atanipa haki yangu; tuzo la kazi yangu liko kwa Mungu. Lakini asema sasa Mwenyezi-Mungu, ambaye aliniita tangu tumboni mwa mama yangu ili nipate kuwa mtumishi wake; nilirudishe taifa la Yakobo kwake, niwakusanye wazawa wa Israeli kwake. Mwenyezi-Mungu amenijalia heshima mbele yake. Mungu wangu amekuwa ndiye nguvu yangu. Yeye asema: “Haitoshi tu wewe kuwa mtumishi wangu, uyainue makabila ya Yakobo, na kurekebisha watu wa Israeli waliobaki. Nitakufanya uwe mwanga wa mataifa, niwaletee wokovu watu wote duniani.” Mwenyezi-Mungu, Mkombozi na Mtakatifu wa Israeli, amwambia hivi yule anayedharauliwa mno, yule anayechukiwa na mataifa, na ambaye ni mtumishi wa watawala: “Wafalme watakuona nao watasimama kwa heshima, naam, wakuu watainama na kukusujudia kwa sababu yangu mimi Mwenyezi-Mungu ambaye hutimiza ahadi zangu; kwa sababu yangu mimi Mtakatifu wa Israeli ambaye nimekuteua wewe.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nilikujibu ombi lako; wakati wa wokovu nilikusaidia. Nimekuweka na kukufanya uwe kiungo cha agano langu na mataifa yote: Kuirekebisha nchi iliyoharibika, na kuwarudishia wenyewe ardhi hiyo; kuwaambia wafungwa, ‘Tokeni humo gerezani’, na wale walio gizani, ‘Njoni nje mwangani!’ Kila mahali watakapokwenda watapata chakula hata kwenye vilima vitupu watapata malisho. Hawataona tena njaa wala kuwa na kiu. Upepo wa hari wala jua havitawachoma, mimi niliyewahurumia nitawaongoza na kuwapeleka kwenye chemchemi za maji. Milima yote nitaifanya kuwa njia, na barabara zangu kuu nitazitengeneza. Watu wangu watarudi kutoka mbali, wengine kutoka kaskazini na magharibi, wengine kutoka upande wa kusini.” Imbeni kwa furaha, enyi mbingu! Shangilia ewe dunia. Pazeni sauti mwimbe enyi milima, maana Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake, naam, atawaonea huruma watu wake wanaoteseka. Wewe Siyoni wasema: “Mwenyezi-Mungu ameniacha; hakika Bwana wangu amenisahau.” Lakini Mwenyezi-Mungu asema: “Je, mama aweza kumsahau mwanawe anayenyonya, asimwonee huruma mtoto wa tumbo lake? Hata kama mama aweza kumsahau mwanawe, mimi kamwe sitakusahau. Nimekuchora katika viganja vyangu; kuta zako naziona daima mbele yangu. Watakaokujenga upya wanakuja haraka, wale waliokuharibu wanaondoka. Inua macho uangalie pande zote; watu wako wote wanakusanyika na kukujia. Naapa kwa nafsi yangu mimi Mwenyezi-Mungu, watu wako watakuwa kwako kama mapambo, utawafurahia kama afanyavyo bibi arusi na utaji wake. “Kweli umekumbana na uharibifu, makao yako yamekuwa matupu, na nchi yako imeteketezwa. Lakini sasa itakuwa ndogo mno kwa wakazi wake; na wale waliokumaliza watakuwa mbali. Wanao waliozaliwa uhamishoni, watakulalamikia wakisema: ‘Nchi hii ni ndogo mno; tupatie nafasi zaidi ya kuishi.’ Hapo ndipo utakapojiuliza mwenyewe: ‘Nani aliyenizalia watoto wote hawa? Nilifiwa na wanangu bila kupata wengine. Nilipelekwa uhamishoni na kutupwa mbali; nani basi aliyewalea watoto hawa? Mimi niliachwa peke yangu, sasa, hawa wametoka wapi?’” Bwana Mungu asema hivi: “Nitayapungia mkono mataifa; naam, nitayapa ishara, nayo yatawabeba watoto wenu wa kiume, kadhalika na watoto wenu wa kike na kuwarudisha kwako. Wafalme watakushughulikia, na malkia watakutengenezea chakula. Watakusujudia na kukupa heshima, na kuramba vumbi iliyo miguuni pako. Hapo utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu; wote wanaonitegemea hawataaibika.” Watu wa Yerusalemu walalamika: “Je, shujaa aweza kunyanganywa nyara zake? Au mateka wa mtu katili waweza kuokolewa?” Mwenyezi-Mungu ajibu: “Naam! Hata nyara za shujaa zitachukuliwa, mateka wa mtu katili wataokolewa. Mimi mwenyewe nitawakabili maadui zako, mimi mwenyewe nitawaokoa watoto wako. Nitawafanya wanaokukandamiza watafunane; watalewa damu yao wenyewe kama divai. Hapo binadamu wote watatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mwokozi wako, mimi ni Mkombozi wako, Mwenye Nguvu wa Yakobo.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kama nimempa talaka mama yako Yerusalemu, hati ya talaka iko wapi? Au kama niliwauza utumwani, yuko wapi basi, huyo niliyemwuzia? Kumbukeni mliuzwa utumwani kwa maovu yenu, mama yenu alifukuzwa kwa makosa yenu. “Nilipokuja kwa nini sikukuta mtu? Nilipoita mbona hamkuitikia? Je, mkono wangu ni mfupi nisiweze kuwaokoeni? Je, sina nguvu ya kuwakomboa? Tazama! Kwa kuikemea kidogo bahari hukauka, na mito nikaifanya kuwa jangwa, samaki wake wakafa na kunuka kwa kukosa maji. Mimi hulivika anga giza, na kulivalisha vazi la kuomboleza.” Bwana Mungu amenipa ufasaha wa lugha, niwatie moyo wale waliochoka. Kila asubuhi hunipa hamu ya kusikiliza anayotaka kunifunza. Bwana Mungu amenifanya msikivu, nami sikuwa mkaidi wala kugeuka mbali naye. Mgongo wangu niliwaachia walionipiga, mashavu yangu waliozingoa ndevu zangu; walioniaibisha na kunitemea mate, sikujificha mbali nao. Bwana Mungu hunisaidia, kwa hiyo siwezi kufadhaika. Uso wangu nimeukaza kama jiwe; najua kwamba sitaaibishwa. Mtetezi wangu yuko karibu. Ni nani atakayepingana nami? Na aje tusimame mahakamani. Adui yangu ni nani? Na ajitokeze mbele basi. Tazama Bwana Mungu hunisaidia. Ni nani awezaye kusema nina hatia? Maadui zangu wote watachakaa kama vazi, nondo watawatafuna. Nani kati yenu amchaye Mwenyezi-Mungu? Nani anayetii maneno ya mtumishi wake? Kama yupo atembeaye gizani bila taa, amtumainie Mwenyezi-Mungu, na kumtegemea Mungu wake. Lakini nyinyi mnaowasha moto, na kujifanyia silaha za mienge, tembeeni kwa mwanga wa moto huo, miali ya moto mliowasha nyinyi wenyewe. Mtakachopata kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ni hiki: Nyinyi mtalala chini na mateso makali. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nisikilizeni enyi mnaotaka kukombolewa, nyinyi mnaonitafuta mimi Mwenyezi-Mungu. Utazameni mwamba mlimochongwa, chimbo la mawe mlimochimbuliwa. Mkumbukeni Abrahamu babu yenu, na Sara aliyewazaa nyinyi. Abrahamu alikuwa hana mtoto wakati nilipomwita, lakini nilimbariki na kumfanya kuwa na wengi. “Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji mji wa Siyoni, nitaparekebisha mahali pake pote palipoharibika. Nyika zake nitazifanya kama bustani ya Edeni, majangwa yake kama bustani ya Mwenyezi-Mungu. Kwake kutapatikana furaha na shangwe, na nyimbo za shukrani zitasikika humo. “Nisikilizeni enyi watu wangu, nitegeeni sikio enyi taifa langu. Sheria na haki zitatoka kwangu mimi; nazo zitakuwa mwanga wa mataifa. Nitaleta ukombozi hima; wokovu nitakaoleta waanza kutokea. Mimi mwenyewe nitayatawala mataifa. Wakazi wa nchi za mbali wananingojea, wanaitegemea nguvu yangu. Inueni macho mzitazame mbingu, kisha tazameni dunia huko chini. Mbingu zitatoweka kama moshi, dunia itachakaa kama vazi, na wakazi wake watakufa kama wadudu. Lakini wokovu niuletao wadumu milele; ukombozi wangu kamwe hautakoma. “Nisikilizeni enyi mjuao mambo ya haki, ambao sheria zangu zimo mioyoni mwenu. Msiogope dharau za watu, wala kufadhaishwa na masimango yao. Maana wataliwa na nondo kama vile vazi; viwavi watawala kama walavyo nguo ya sufu. Lakini ukombozi niletao mimi utadumu milele; wokovu wangu hautakuwa na mwisho.” Amka! Amka ee Mwenyezi-Mungu! Jivike nguvu zako utuokoe. Amka kama ulivyofanya hapo zamani, nyakati za vizazi vya hapo kale. Je, si wewe uliyemkatakata Rahabu, ukalitumbua dude hilo la kutisha? Wewe ndiwe uliyeikausha bahari, ndiwe uliyevikausha vilindi vya maji, ukafanya njia katika vilindi vya bahari, ili wale uliowakomboa wavuke humo. Watu wako uliowakomboa, ee Mwenyezi-Mungu, watarudi, watakuja Siyoni wakiimba; watajaa furaha ya milele, watapata furaha na shangwe. Huzuni na maombolezo vitatoweka kabisa. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi, naam mimi, ndimi ninayekufariji. Kwa nini wewe unamwogopa mtu ambaye hufa, binadamu ambaye hutoweka kama nyasi? Wewe umenisahau mimi Mwenyezi-Mungu Muumba wako, niliyezitandaza mbingu, na kuiweka misingi ya dunia! Wewe waendelea kuogopa siku zote, kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu wako, kwamba yuko tayari kukuangamiza! Lakini hasira yake itafika wapi? Wanaodhulumiwa watafunguliwa hima, hawatakufa na kushuka shimoni, wala hawatatindikiwa chakula. Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; nivurugaye bahari, mawimbi yake yakanguruma; Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndilo jina langu! Nimeyaweka maneno yangu mdomoni mwako; nimekuficha katika kivuli cha mkono wangu. Mimi nilizitandaza mbingu, nikaiweka misingi ya dunia. Mimi nawaambieni enyi watu wa Siyoni: ‘Nyinyi ni watu wangu.’” Amka ewe Yerusalemu! Amka usimame wima! Mwenyezi-Mungu amekunywesha kikombe cha ghadhabu yake, nawe umeinywa mpaka tone la mwisho, mpaka ukayumbayumba. Kati ya watoto wote uliowazaa hakuna yeyote wa kukuongoza. Hakuna hata mmoja wa kukushika mkono kati ya watoto wote uliowalea. Majanga haya mawili yamekupata: Uharibifu na maangamizi; njaa na mauaji. Nani atakayekuonea huruma? Nani atakayekufariji? Watoto wako wamezirai, wamelala pembeni mwa kila barabara, wako kama paa aliyenaswa wavuni. Wamepatwa na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu, wamepatwa na adhabu ya Mungu wako. Basi, sikiliza ewe Yerusalemu unayeteseka; sikiliza wewe uliyelewa, lakini sio kwa divai. Bwana, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, awateteaye watu wake, asema hivi: “Nimekuondolea kikombe cha kuyumbisha, hutakunywa tena kikombe cha ghadhabu yangu. Nitawanywesha watesi wako kikombe hicho waliokuambia ulale chini wapite juu yako; wakaufanya mgongo wako kama ardhi, kama barabara yao ya kupitia.” Amka! Amka! Jipe nguvu zako ewe mji wa Siyoni! Jivike mavazi yako mazuri, ewe Yerusalemu, mji mtakatifu. Maana hawataingia tena kwako watu wasiotahiriwa na walio najisi. Jikungute mavumbi, uinuke ewe Yerusalemu uliyetekwa nyara! Jifungue minyororo yako shingoni, ewe binti Siyoni uliyechukuliwa mateka. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi mliuzwa utumwani bila malipo yoyote, na mtakombolewa bila kulipa hata senti moja. Tena mwanzoni nyinyi watu wangu mlikimbilia Misri mkakaa huko. Halafu baadaye Waashuru waliwakandamiza bila sababu yoyote. Katika hali ya sasa napata faida gani kuwaona watu wangu wamepelekwa utumwani? Hao wanaowatawala wanajitapa. Nalo jina langu laendelea kudharauliwa kila siku. Kwa hiyo watu wangu watajua mimi ni nani; siku hiyo watajua kwamba ni mimi ninayesema: Niko!” Tazama inavyopendeza kumwona mjumbe akitokea mlimani, ambaye anatangaza amani, ambaye analeta habari njema, na kutangaza ukombozi! Anauambia mji wa Siyoni: “Mungu wako anatawala!” Sikiliza sauti ya walinzi wako; wanaimba pamoja kwa furaha, maana wanaona kwa macho yao wenyewe, kurudi kwa Mwenyezi-Mungu mjini Siyoni. Pazeni sauti za shangwe, enyi magofu ya Yerusalemu! Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake, ameukomboa mji wa Yerusalemu. Mwenyezi-Mungu ameonesha nguvu yake tukufu, mbele ya mataifa yote. Atawaokoa watu wake, na ulimwengu wote utashuhudia. Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa; msiguse kitu chochote najisi! Ondokeni huku Babuloni! Jitakaseni enyi mbebao vyombo vya Mwenyezi-Mungu. Safari hii hamtatoka kwa haraka, wala hamtaondoka mbiombio! Maana Mwenyezi-Mungu atawatangulieni, Mungu wa Israeli atawalinda kutoka nyuma. Mungu asema hivi: “Mtumishi wangu atafanikiwa; atatukuzwa na kupewa cheo, atapata heshima kuu. Wengi waliomwona walishtuka, kwa vile sura yake ilikuwa imeharibiwa; hakuwa tena na umbo la kibinadamu! Lakini sasa ameyashangaza mataifa mengi. Wafalme wanaduwaa kwa sababu yake, maana wataona mambo ambayo hawajapata kuambiwa, na kufahamu mambo ambayo hawajapata kusikia.” Nani aliyeamini mambo tuliyosikia? Nani aliyetambua kuwa mkono wa Mwenyezi-Mungu ulihusika? Maana, mbele yake Mwenyezi-Mungu, mtumishi wake alikua kama mti mchanga, kama mzizi katika nchi kavu. Hakuwa na umbo wala sura ya kutupendeza, wala hakuwa na uzuri wowote wa kutuvutia. Alidharauliwa na kukataliwa na watu, alikuwa mtu wa uchungu na huzuni. Alikuwa kama mtu kinyaa kwa watu; alidharauliwa na tukamwona si kitu. Hata hivyo alivumilia majonzi yetu, na kubeba huzuni zetu. Sisi tulifikiri amepata adhabu, amepigwa na Mungu na kuteswa. Lakini alijeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu, aliumizwa kwa sababu ya maovu yetu. Kwa kuadhibiwa kwake sisi tumepata uhai; kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote tumepotea kama kondoo, kila mmoja wetu ameelekea njia yake. Lakini Mwenyezi-Mungu alimtwika adhabu, ambayo sisi wenyewe tuliistahili. Alidhulumiwa na kuteswa, lakini alivumilia kwa unyenyekevu, bila kutoa sauti hata kidogo. Alikuwa kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni, kama kondoo akaavyo kimya anapokatwa manyoya. Hakutoa sauti hata kidogo. Alidhulumiwa, akahukumiwa na kupelekwa kuuawa; na hakuna mtu aliyejali yanayompata. Alifukuzwa kutoka nchi ya walio hai, kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Walimzika pamoja na wahalifu; katika kifo aliwekwa pamoja na matajiri, ingawa hakutenda ukatili wowote, wala hakusema neno lolote la udanganyifu. Mwenyezi-Mungu alipenda kumwumiza na kumweka katika huzuni. Alijitoa mhanga kwa ajili ya kuondoa dhambi. Mtumishi wa Mungu atakuwa na wazawa; ataishi maisha marefu. Yeye ndiye atakayetimiza mpango wa Mwenyezi-Mungu. Mungu asema: “Baada ya kutaabika sana, mtumishi wangu atafurahi. Kwa kuwajibika kwake kikamilifu, atatosheka na matokeo hayo. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwadilifu atawafanya wengi wawe waadilifu Yeye atazibeba dhambi zao. Kwa hiyo, nitamweka katika cheo cha wakuu, atagawa nyara pamoja na wenye nguvu; kwa kuwa alijitolea mwenyewe kufa, akawekwa katika kundi moja na wakosefu, alizibeba dhambi za watu wengi, akawaombea msamaha hao wakosefu.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Imba kwa shangwe ewe uliye tasa, wewe ambaye hujapata kuzaa! Paza sauti na kuimba kwa nguvu, wewe usiyepata kujifungua mtoto. Maana watoto wako wewe uliyeachwa watakuwa wengi kuliko wa aliye na mume. Panua nafasi hemani mwako, tandaza mapazia hapo unapoishi, usijali gharama zake. Zirefushe kamba zake, na kuimarisha vigingi vyake; maana utapanuka kila upande; wazawa wako watamiliki mataifa, miji iliyokuwa mahame itajaa watu. Usiogope maana hutaaibishwa tena; usifadhaike maana hutadharauliwa tena. Utaisahau aibu ya ujana wako, wala hutaikumbuka tena fedheha ya ujane wako. Muumba wako atakuwa mume wako; Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndilo jina lake, Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; yeye aitwa ‘Mungu wa ulimwengu wote’. “Yerusalemu, Mwenyezi-Mungu amekuita tena wewe kama vile mke aliyeachwa na kuhuzunika, mke aliyeolewa akiwa kijana akaachwa. Mungu wako anasema: Nilikuacha kwa muda mfupi tu; kwa huruma nyingi, nitakurudisha. Kwa hasira nyingi nilikuficha uso wangu kwa kitambo, lakini kwa fadhili za milele nitakuonea huruma. Mimi Mwenyezi-Mungu Mkombozi wako, nimesema. “Nitafanya kama nilivyofanya wakati wa Noa: Wakati ule niliapa kwamba sitaifunika tena ardhi kwa gharika. Basi sasa naapa kwamba sitakukasirikia tena wala sitakukemea tena. Milima yaweza kutoweka, vilima vyaweza kuondolewa, lakini fadhili zangu hazitakuondoka, agano langu la amani halitaondolewa. Mimi Mwenyezi-Mungu nikuhurumiaye nimesema. “Ewe Yerusalemu uliyeteseka, uliyetaabishwa na kukosa wa kukufariji! Nitakujenga upya kwa mawe ya thamani, misingi yako itakuwa ya johari ya rangi ya samawati. Minara yako nitaijenga kwa mawe ya akiki, malango yako kwa almasi, na ukuta wako kwa mawe ya thamani. “Watu wako watafunzwa nami Mwenyezi-Mungu, wanao watapata ustawi mwingi. Utaimarika katika uadilifu, utakuwa mbali na dhuluma, nawe hutaogopa kitu; utakuwa mbali na hofu, maana haitakukaribia. Mtu yeyote akija kukushambulia, hatakuwa ametumwa nami. Yeyote atakayekushambulia, ataangamia mbele yako. “Tazama, mimi ndiye niliyemuumba mhunzi, afukutaye moto wa makaa na kufua silaha. Ni mimi pia niliyemuumba mwangamizi anayeangamiza. Silaha zote zilizoundwa kukudhuru wewe hazitafaa chochote kile. Mtu akikushtaki mahakamani, utamshinda. Hilo ndilo fungu nililowapangia watumishi wangu. Hizo ndizo haki nilizowathibitishia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Haya! Kila mwenye kiu na aje kwenye maji! Njoni, nyote hata msio na fedha; nunueni ngano mkale, nunueni divai na maziwa. Bila fedha, bila gharama! Mbona mnatumia fedha yenu kwa ajili ya kitu kisicho chakula? Ya nini kutoa jasho lenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni mimi kwa makini, nanyi mtakula vilivyo bora, na kufurahia vinono. “Tegeni sikio enyi watu wangu, mje kwangu; nisikilizeni, ili mpate kuishi. Nami nitafanya nanyi agano la milele; nitawapeni fadhili nilizomwahidi Daudi. Mimi nilimfanya kiongozi na kamanda wa mataifa ili yeye anishuhudie kwa watu wa mataifa. Sasa utayaita mataifa usiyoyajua, watu wa mataifa yasiyokutambua watakujia mbio, kwa sababu yangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; kwa sababu yangu mimi Mtakatifu wa Israeli niliyekufanya wewe utukuke.” Mtafuteni Mwenyezi-Mungu wakati bado anapatikana, mwombeni msaada wakati yupo bado karibu. Waovu na waache njia zao mbaya, watu wabaya waachane na mawazo yao mabaya; wamrudie Mwenyezi-Mungu apate kuwahurumia, wamwendee Mungu wetu maana atawasamehe. Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mawazo yangu si kama mawazo yenu, wala njia zangu si kama njia zenu. Kama vile mbingu zilivyo mbali na dunia, ndivyo njia zangu zilivyo mbali na zenu, na mawazo yangu mbali na mawazo yenu. “Kama vile mvua na theluji ishukavyo toka mbinguni, wala hairudi huko bali huinywesha ardhi, ikaifanya ichipue mimea ikakua, ikampatia mpanzi mbegu na kuwapa watu chakula, vivyo hivyo na neno langu mimi: Halitanirudia bila mafanikio, bali litatekeleza matakwa yangu, litafanikiwa lengo nililoliwekea. “Mtatoka Babuloni kwa furaha; mtaongozwa mwende kwa amani. Milima na vilima mbele yenu vitapaza sauti na kuimba, na miti yote mashambani itawapigia makofi. Badala ya michongoma kutamea misonobari, na badala ya mbigili kutamea mihadasi. Hilo litakuwa jambo litakalowakumbusha watu juu ya mambo niliyotenda mimi Mwenyezi-Mungu; ishara ya milele ambayo haitafutwa.” Mwenyezi-Mungu asema: “Zingatieni haki na kutenda mema, maana nitawaokoeni hivi karibuni, watu wataona wazi kwamba ninawakomboeni. Heri mtu anayezingatia kikamilifu ninayosema, anayeshika sheria ya Sabato kwa heshima na kuepa kutenda uovu wowote. “Mgeni anayenitambua mimi Mwenyezi-Mungu asifikiri: ‘Hakika Mwenyezi-Mungu atanitenga na watu wake.’ Naye towashi asiseme: ‘Mimi ni mti mkavu tu!’ Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema: Towashi ashikaye sheria zangu za Sabato, anayefanya mambo yanayonipendeza, na kulizingatia agano langu, nitampa nafasi maalumu na ya sifa katika nyumba yangu na kuta zake; nafasi bora kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike: Nitampa jina la kukumbukwa daima, na ambalo halitafutwa kamwe. “Watu wageni watakaonikiri mimi Mwenyezi-Mungu, watakaoniheshimu, wakapenda jina langu na kuwa watumishi wangu, wote watakaoshika Sabato bila kuikufuru, watu watakaozingatia agano langu, hao nitawaleta katika mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; tambiko na sadaka zao zitakubaliwa madhabahuni pangu. Maana nyumba yangu itaitwa: ‘Nyumba ya sala kwa ajili ya watu wote’. “Hii ni kauli yangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu ninayewakusanya Waisraeli waliotawanyika. Licha ya hao niliokwisha kukusanya, nitawakusanya watu wengine wajumuike nao.” Enyi wanyama wote wakali, nanyi wanyama wote wa mwituni, njoni muwatafune watu wangu. Maana viongozi wao wote ni vipofu; wote hawana akili yoyote. Wote ni kama mbwa bubu wasiobweka, hulala tu na kuota ndoto, hupenda sana kusinzia! Hao ni kama mbwa wenye uchu sana, wala hawawezi kamwe kutoshelezwa. Wachungaji hao hawana akili yoyote; kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe. Huambiana, “Njoni, twende kutafuta divai; njoni tunywe tushibe pombe! Kesho itakuwa kama leo, tena itakuwa sikukuu kubwa zaidi.” Mtu mwadilifu akifa, hakuna mtu anayejali; mtu mwema akifariki, hakuna mtu anayefikiri na kusema: “Mtu huyo mwema ameondolewa asipatwe na maafa, ili apate kuingia kwenye amani.” Watu wanaofuata njia ya haki, watakuwa na amani na kupumzika. Lakini Mwenyezi-Mungu asema: “Njoni hapa nyinyi wana wa wachawi; nyinyi wazawa wa wachawi, wazinzi na malaya. Je, mnadhani mnamdhihaki nani? Mnamfyonya nani na kumtolea ulimi? Nyinyi wenyewe ni wahalifu tangu mwanzo, nyinyi ni kizazi kidanganyifu. Nyinyi mnawaka tamaa kwenye miti ya mialoni, na katika kila mti wa majani mabichi. Mnawachinja watoto wenu na kuwatambika katika mabonde na nyufa za majabali. Mnachagua mawe laini mabondeni, na kuyafanya kitovu cha maisha yenu. Mnayamiminia tambiko ya kinywaji na kuyapelekea tambiko ya nafaka! Je, mimi nitaridhishwa kwa vitu hivyo? Mmeweka vitanda vyenu juu ya milima mikubwa, na kwenda huko kutoa tambiko. Nyuma ya milango na miimo mmetundika kinyago chenu. Nyinyi mnaniacha mimi na kutandika na kuvipanua vitanda vyenu. Mnafanya mapatano na hao mliopenda vitanda vyao. Humo mnazitosheleza tamaa zenu mbaya, huku mnakodolea macho kinyago chenu. Mnajitia marashi na manukato kwa wingi kisha mnakwenda kumwabudu Moleki. Mnawatuma wajumbe wenu huko na huko, kujitafutia miungu ya kuabudu; hata kuzimu walifika. Mlichoshwa na safari zenu ndefu, hata hivyo hamkukata tamaa; mlijipatia nguvu mpya, ndiyo maana hamkuzimia. “Mlimwogopa na kutishwa na nani hata mkasema uongo, mkaacha kunikumbuka mimi na kuacha kabisa kunifikiria? Mimi sikuwaambia kitu kwa muda mrefu; ndio maana labda mkaacha kuniheshimu! Mnafikiri mnafanya sawa, lakini nitayafichua matendo yenu, nayo miungu yenu haitawafaa kitu. Mtakapolia kuomba msaada, rundo la vinyago vyenu na liwaokoe! Upepo utavipeperushia mbali; naam, pumzi itavitupilia mbali. Lakini watakaokimbilia usalama kwangu, wataimiliki nchi, mlima wangu mtakatifu utakuwa mali yao.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Jengeni! Jengeni! Tayarisheni njia! Ondoeni vikwazo vyote njiani mwa watu wangu!” Hivi ndivyo asemavyo Mungu aliye juu kabisa, aishiye milele na ambaye jina lake ni “Mtakatifu”: “Mimi nakaa huko juu, mahali patakatifu, nakaa pia na wenye majuto na wanyenyekevu. Mimi nitawatia moyo walio wanyenyekevu na kuwapa nguvu wenye majuto. Maana sitaendelea kuwalaumu wala kuwakasirikia daima. La sivyo hao niliowaumba watadhoofika mbele yangu, nami ndiye niliyewapa pumzi yangu ya uhai. Niliwakasirikia kwa sababu ya uovu na tamaa zao; niliwaadhibu, nikauficha uso wangu na kukasirika. Lakini wao waliendelea kufuata njia zao wenyewe. Niliiona mienendo yao, lakini nitawaponya; nitawaongoza na kuwapa faraja, nitawatuliza hao wanaoomboleza. Mimi nitawapa amani, amani kwa walio mbali na walio karibu! Mimi nitawaponya. Lakini waovu ni kama bahari iliyochafuka, ambayo haiwezi kutulia; mawimbi yake hutupa tope na takataka.” Mungu wangu asema hivi: “Watu waovu sitawapa amani.” Mwenyezi-Mungu asema: “Piga kelele, wala usijizuie; paza sauti yako kama tarumbeta. Watangazie watu wangu makosa yao, waambie wazawa wa Yakobo dhambi zao. Siku hata siku wananijia kuniabudu, wanatamani kujua mwongozo wangu, kana kwamba wao ni taifa litendalo haki, taifa lisilosahau sheria za Mungu wao. Wananitaka niamue kwa haki, na kutamani kukaa karibu na Mungu. “Nyinyi mnaniuliza: ‘Mbona tunafunga lakini wewe huoni? Mbona tunajinyenyekesha, lakini wewe hujali?’ “Ukweli ni kwamba wakati mnapofunga, mnatafuta tu furaha yenu wenyewe, na kuwakandamiza wafanyakazi wenu! Mnafunga, na kugombana na kupigana ngumi. Mkifunga namna hiyo maombi yenu hayatafika kwangu juu. Mfungapo, nyinyi mnajitaabisha; mnaviinamisha vichwa vyenu kama unyasi, na kulalia nguo za magunia na majivu. Je, huo ndio mnaouita mfungo? Je, hiyo ni siku inayokubaliwa nami? “La! Mfungo ninaotaka mimi ni huu: Kuwafungulia waliofungwa bila haki, kuziondoa kamba za utumwa, kuwaachia huru wanaokandamizwa, na kuvunjilia mbali udhalimu wote! Mfungo wa kweli ni kuwagawia wenye njaa chakula chako, kuwakaribisha nyumbani kwako maskini wasio na makao, kuwavalisha wasio na nguo, bila kusahau kuwasaidia jamaa zenu. “Mkifanya hivyo mtangara kama pambazuko, mkiwa wagonjwa mtapona haraka. Matendo yenu mema yatawatangulia, nami nitawalindeni kutoka nyuma kwa utukufu wangu. Ndipo mtakapoomba, nami Mwenyezi-Mungu nitawaitikia; mtalia kwa sauti kuomba msaada, nami nitajibu, ‘Niko hapa!’ “Kama mkiiondoa dhuluma kati yenu, mkiacha kudharau wengine na kusema maovu, mkiwapa chakula kwa ukarimu wenye njaa, mkitosheleza mahitaji ya wenye dhiki, mwanga utawaangazia nyakati za giza, giza lenu litakuwa kama mchana. Mimi Mwenyezi-Mungu nitawaongozeni daima, nitatosheleza mahitaji yenu wakati wa shida. Nitawaimarisha mwilini, nanyi mtakuwa kama bustani iliyomwagiliwa maji, kama chemchemi ya maji ambayo maji yake hayakauki kamwe. Magofu yenu ya kale yatajengwa; mtajenga upya juu ya misingi iliyoachwa zamani. Nanyi mtaitwa watu waliotengeneza upya kuta, watu waliozifanya barabara za mji zipitike tena. “Kama ukiacha kufanya kazi siku ya Sabato, ukaacha shughuli zako siku yangu hiyo takatifu; kama ukiifanya siku yangu kuwa ya furaha, ukaiheshimu siku hiyo takatifu ya Mwenyezi-Mungu, ukaacha na shughuli zako na kupiga domo, utapata furaha yako kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, nitakupatia ushindi katika kila pingamizi nchini, nitakulisha mali ya Yakobo, babu yako. Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema.” Msifikiri mkono wa Mungu ni mfupi, hata asiweze kuwaokoeni; au masikio yake yamezibika, hata asiweze kuwasikieni. Dhambi zenu ndizo zinazowatenga na Mungu wenu, dhambi zenu zimemfanya ajifiche mbali nanyi hata asiweze kuwasikieni. Maana mikono yenu imetiwa najisi kwa mauaji, na vidole vyenu kwa matendo maovu. Midomo yenu imesema uongo, na ndimi zenu husema uovu. Hakuna atoaye madai yake kwa haki, wala anayeshtaki kwa uaminifu. Mnategemea hoja batili; mnasema uongo. Mnatunga hila na kuzaa uovu. Mnaangua mayai ya joka lenye sumu, mnafuma utando wa buibui. Anayekula mayai yenu hufa, na yakipasuliwa nyoka hutokea. Utando wenu haufai kwa mavazi, watu hawawezi kujifunikia mnachofuma. Kazi zenu ni kazi za uovu, matendo yenu yote ni ukatili mtupu. Mko mbioni kutenda maovu, mnaharakisha kumwaga damu isiyo na hatia. Mawazo yenu ni mawazo ya uovu, popote mwendapo mnaacha ukiwa na uharibifu. Njia ya amani hamwijui kamwe; njia zenu zote ni za dhuluma. Mmejifanyia njia potovu, yeyote anayepitia humo hapati amani. Ndio maana haki iko mbali nasi, maongozi ya uadilifu hayapo kwetu. Tunatazamia kupata mwanga kumbe ni giza tupu, twatazamia mwangaza, lakini twatembea gizani. Kama vipofu twapapasapapasa ukuta; tunasitasita kama watu wasio na macho. Tunajikwaa mchana kana kwamba ni usiku, miongoni mwa wenye nguvu sisi ni kama wafu. Twanguruma kama dubu, twaomboleza tena na tena kama hua. Twatazamia hukumu ya haki, lakini haipo, twatazamia wokovu, lakini uko mbali nasi. Makosa yetu mbele yako ni mengi mno, dhambi zetu zashuhudia dhidi yetu. Naam, makosa yetu tunaandamana nayo, tunayajua maovu yetu. Tumekuasi na kukukana ee Mwenyezi-Mungu, tumekataa kukufuata ewe Mungu wetu. Udhalimu na uasi ndivyo tunavyopania, mioyoni mwetu twatunga na kutoa maneno ya uongo. Haki imewekwa kando, uadilifu uko mbali; ukweli unakanyagwa mahakamani, uaminifu haudiriki kuingia humo. Ukweli umekosekana, naye anayeacha uovu hunyanyaswa. Mungu aliona mambo hayo, akachukizwa, alichukizwa kwamba hakuna haki. Aliona kwamba hakuna mtu aliyejali, akashangaa kwamba hakuna aliyeingilia kati. Basi akaamua kunyosha mkono wake mwenyewe, uadilifu wake ukamhimiza. Alivaa uadilifu kama vazi la kujikinga kifuani, na wokovu kama kofia ya chuma kichwani. Atajivika kisasi kama vazi, na kujifunika wivu kama joho. Atawaadhibu maadui kadiri ya matendo yao, naam, ghadhabu yake na kisasi vitawapata maadui zake; atawaadhibu hata wakazi wa nchi za mbali. Toka magharibi hadi mashariki, kila mtu atamcha Mwenyezi-Mungu na kutambua utukufu wake. Maana atakuja kama mto uendao kasi, mto unaosukumwa kwa upepo wa Mwenyezi-Mungu. Naye atakuja Siyoni kama Mkombozi, Mkombozi wa wazawa wa Yakobo ambao wataachana na makosa yao. Asema Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu asema: “Mimi nafanya nanyi agano hili: Roho yangu niliyowajazeni, maneno niliyoyaweka mdomoni mwenu, hayataondoka kwenu kamwe, wala kwa watoto na wajukuu zenu, tangu sasa na hata milele.” Inuka ee Siyoni uangaze; maana mwanga unachomoza kwa ajili yako, utukufu wa Mwenyezi-Mungu unakuangaza. Tazama, giza litaifunika dunia, giza nene litayafunika mataifa; lakini wewe, Mwenyezi-Mungu atakuangazia, utukufu wake utaonekana kwako. Mataifa yataujia mwanga wako, wafalme waujia mwanga wa pambazuko lako. Inua macho utazame pande zote; wote wanakusanyika waje kwako. Wanao wa kiume watafika toka mbali, wanao wa kike watabebwa mikononi. Utaona na uso wako utangara, moyo wako utasisimka na kushangilia. Maana utajiri wa bahari utakutiririkia, mali za mataifa zitaletwa kwako. Makundi ya ngamia yataifunika nchi yako, naam, ndama wa ngamia kutoka Midiani na Efa; wote kutoka Sheba watakuja. Watakuletea dhahabu na ubani, wakitangaza sifa za Mwenyezi-Mungu. Makundi ya kondoo wa Kedari yatakusanywa kwako, utaweza kuwatumia kondoo madume wa Nebayothi kuwa kafara; utawatoa kuwa tambiko inayokubalika madhabahuni pa Mungu, naye ataitukuza nyumba yake tukufu. Nani hao wanaopepea kama mawingu, kama njiwa wanaoruka kwenda viotani mwao? Ni meli zitokazo nchi za mbali, zikitanguliwa na meli za Tarshishi. Zinawaleta watoto wako, pamoja na fedha na dhahabu yao, kwa sifa ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, kwa sifa ya Mungu, Mtukufu wa Israeli, maana amewafanya mtukuke. Mwenyezi-Mungu asema: “Wageni watazijenga upya kuta zako, wafalme wao watakutumikia. Maana kwa hasira yangu nilikupiga, lakini kwa fadhili yangu nimekuhurumia. Malango yako yatakuwa wazi daima; usiku na mchana hayatafungwa, ili watu wakuletee utajiri wa mataifa, pamoja na wafalme wao katika maandamano. Kila ufalme au taifa lisilokutumikia litaangamia; mataifa hayo yatatokomezwa kabisa. “Utaletewa fahari ya msitu wa Lebanoni: Mbao za miberoshi, mivinje na misonobari, zitumike kupamba mahali pa maskani yangu; nami nitaparembesha hapo ninapokaa. Wazawa wa wale waliokudhulumu, watakuja na kukuinamia kwa heshima. Wote wale waliokudharau, watasujudu mbele ya miguu yako. Watakuita: ‘Mji wa Mwenyezi-Mungu’, ‘Siyoni, Mji wa Mtakatifu wa Israeli’. “Wewe ulikuwa umeachwa na kuchukiwa, hakuna aliyependa hata kupitia kwako. Lakini sasa nitakufanya uwe na fahari milele, utakuwa mji wa furaha kizazi hata kizazi. Utaletewa chakula na watu wa mataifa, naam, wafalme watakupatia chakula bora. Hapo utatambua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ni Mwokozi wako; mimi Mwenye Nguvu wa Yakobo ni Mkombozi wako. “Badala ya shaba nitakuletea dhahabu, badala ya chuma nitakuletea fedha, badala ya miti, nitakuletea shaba, na badala ya mawe nitakuletea chuma. Amani itatawala juu yako, uadilifu utakuongoza. Ukatili hautasikika tena nchini mwako; wala uharibifu na maangamizi ndani ya mipaka yako. Utaweza kuziita kuta zako: ‘Wokovu’, na malango yako: ‘Sifa’. “Hutahitaji tena jua kukuangazia mchana, wala mwezi kukumulikia usiku; maana mimi Mwenyezi-Mungu ni mwanga wako milele; mimi Mungu wako nitakuwa fahari yako. Mwanga wako mchana hautatua kama jua, wala mwangaza wako usiku kufifia kama mbalamwezi; maana Mwenyezi-Mungu ni mwanga wako milele, nazo siku zako za kuomboleza zitakoma. Watu wako wote watakuwa waadilifu, nao wataimiliki nchi milele. Hao ni chipukizi nililopanda mimi, kazi ya mikono yangu kwa ajili ya utukufu wangu. Aliye mdogo kati yenu atakuwa ukoo, aliye mdogo kuliko wote atakuwa taifa kubwa. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu; wakati ufikapo nitayatekeleza hayo haraka.” Bwana Mwenyezi-Mungu amenijaza roho yake, maana Mwenyezi-Mungu ameniweka wakfu, akanituma niwaletee wanaokandamizwa habari njema, niwatibu waliovunjika moyo, niwatangazie mateka kwamba watapata uhuru, na wafungwa kwamba watafunguliwa. Amenituma niutangaze mwaka wake wa neema, na siku ya Mungu wetu ya kulipiza kisasi; niwafariji wote wanaoomboleza; niwape wale wanaoomboleza katika Siyoni taji la maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya moyo mzito. Nao wataitwa mialoni madhubuti, aliyopanda Mwenyezi-Mungu kuonesha utukufu wake. Watayajenga upya magofu ya zamani, wataisimika miji iliyoharibiwa hapo kwanza; wataitengeneza miji iliyobomolewa, uharibifu wa vizazi vingi vilivyopita. Wageni watakuwa hapo kuwachungia mifugo yenu; watawalimia na kuwatunzia mizabibu yenu. Nanyi mtaitwa: “Makuhani wa Mwenyezi-Mungu”, Mtaitwa: “Watumishi wake Mungu wetu”. Mtafaidika kwa utajiri wa mataifa, mtatukuka kwa mali zao. Kwa vile mlipata aibu maradufu, watu wakaona kuwa fedheha ni majaliwa yenu, sasa mtapata eneo maradufu kuwa mali yenu, na furaha yenu itadumu milele. “Mimi Mwenyezi-Mungu napenda haki; nachukia unyanganyi na uhalifu. Nitawatuza watu wangu kwa uaminifu, nitafanya nao agano la milele. Wazawa wao watakuwa maarufu kati ya mataifa; watajulikana kuwa maarufu kati ya watu wengine. Kila atakayewaona atakiri kwamba wao ni watu aliowabariki Mwenyezi-Mungu.” Nitafurahi sana kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, nafsi yangu itashangilia kwa sababu ya Mungu wangu. Maana amenivika vazi la wokovu, amenivalisha vazi la uadilifu, kama bwana arusi ajipambavyo kwa shada la maua, kama bibi arusi ajipambavyo kwa johari zake. Hivyo, kama vile ardhi ioteshavyo mimea, na shamba lichipushavyo mbegu zilizopandwa humo, Mwenyezi-Mungu atasababisha uadilifu na sifa kuchomoza mbele ya mataifa yote. Kwa ajili ya Siyoni sitakaa kimya, kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, mpaka kuokolewa kwake kuchomoze kama umeme, wokovu wake utokeze kama mwenge. Mataifa watauona wokovu wako, wafalme wote watauona utukufu wako. Nawe utaitwa kwa jina jipya, jina atakalokupa Mwenyezi-Mungu mwenyewe. Utakuwa taji zuri mkononi mwa Mwenyezi-Mungu; kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako. Hutaitwa tena: “Aliyeachwa”, wala nchi yako haitaitwa: “Ukiwa”. Bali utaitwa: “Namfurahia,” na nchi yako itaitwa: “Aliyeolewa.” Maana Mwenyezi-Mungu amependezwa nawe, naye atakuwa kama mume wa nchi yako. Maana kama kijana mwanamume amwoavyo msichana, ndivyo aliyekujenga atakavyokuwa mume wako. Kama bwana arusi afurahivyo juu ya bibi arusi, ndivyo Mungu atakavyofurahi juu yako. “Juu ya kuta zako ee Yerusalemu nimeweka walinzi, usiku na mchana kamwe hawatakaa kimya.” Enyi mnaomkumbusha Mwenyezi-Mungu ahadi yake, msikae kimya; msimpe hata nafasi ya kupumzika, mpaka atakapousimika mji wa Yerusalemu, na kuufanya uwe fahari ulimwenguni kote. Mwenyezi-Mungu ameapa kwa mkono wake wa kulia, naam, ameapa kwa mkono wake wenye nguvu akisema: “Sitawapa tena maadui zako nafaka yako; wala wageni hawatakunywa tena divai yako ambayo umeitolea jasho. Bali nyinyi mliyoivuna nafaka hiyo, mtaila na kunitukuza mimi Mwenyezi-Mungu. Nyinyi mliochuma zabibu hizo, mtakunywa divai yake katika nyua zangu takatifu.” Wakazi wa Yerusalemu, tokeni, tokeni nje ya mji, watayarishieni njia watu wenu wanaorejea! Jengeni! Jengeni barabara na kuondoa mawe yote! Wekeni alama kwa ajili ya watu. Mwenyezi-Mungu ametangaza duniani kote, waambie watu wa Siyoni: “Mkombozi wenu anakuja, zawadi yake iko pamoja naye na tuzo lake liko mbele yake.” Nyinyi mtaitwa: “Watu Watakatifu”, “Watu waliokombolewa na Mwenyezi-Mungu.” Na Yerusalemu utaitwa: “Mji aupendao Mungu”, “Mji ambao Mungu hakuuacha.” Ni nani huyu ajaye kutoka Edomu, anayefika kutoka Bosra na mavazi ya madoa mekundu? Ni nani huyo aliyevaa mavazi ya fahari, anatembea kwa nguvu zake kubwa? Ni mimi Mwenyezi-Mungu ninayetangaza ushindi wangu; nami ni mwenye nguvu ya kuokoa. Lakini mbona nguo yako ni nyekundu, nyekundu kama ya mtu anayekamua zabibu? “Naam, nimekamua zabibu peke yangu, wala hakuna mtu aliyekuja kunisaidia. Nimeyakanyaga mataifa kwa hasira yangu, niliyapondaponda kwa ghadhabu yangu. Nguo zangu zimejaa madoa ya damu yao, imeyachafua kabisa mavazi yangu. Niliamua kuwa siku ya kulipiza kisasi imefika; wakati wa kuwakomboa watu wangu umefika. Nilitazama na hapakuwa na wa kunisaidia; nilishangaa hapakuwa na wa kuniunga mkono. Lakini nilijipatia ushindi kwa mkono wangu, ghadhabu yangu ilinihimiza. Kwa hasira yangu niliwaponda watu, niliwalewesha kwa ghadhabu yangu; damu yao niliimwaga chini ardhini.” Nitasimulia fadhili za Mwenyezi-Mungu; nitataja matendo yake yote yastahiliyo sifa, kwa sababu ya yote aliyotutendea, wema wake mkuu aliowapa Waisraeli kwa huruma yake, kadiri ya wingi wa fadhili zake. Maana alisema juu yao: “Hakika, hawa ni watu wangu; watoto wangu ambao hawatanidanganya.” Basi yeye akawa Mwokozi wao. Katika taabu zao zote, hakumtuma mjumbe mwingine kuwasaidia, ila yeye mwenyewe alikuja kuwaokoa. kwa upendo na huruma yake aliwakomboa. Aliwabeba na kuwachukua tangu zamani. Lakini wao walikuwa wakaidi, wakaihuzunisha roho yake takatifu. Basi, Mungu akageuka, akawa adui yao; yeye mwenyewe akapigana nao. Ndipo walipokumbuka siku za zamani, wakati wa Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu. Wakauliza, “Yuko wapi sasa Mwenyezi-Mungu, aliyewaokoa wachungaji wa kundi lake baharini? Yuko wapi yule aliyeiweka roho yake takatifu kati yao, ambaye kwa mkono wake wenye nguvu alifanya maajabu kwa njia ya Mose, akapasua bahari na kuwaongoza watu wake, na kujipatia jina la milele? Aliwaongoza katikati ya vilindi vya bahari, wakapita humo kama farasi bila kujikwaa. Kama ng'ombe wapelekwavyo malishoni bondeni, ndivyo roho ya Mungu ilivyowapumzisha watu wake. Ndivyo ee Mungu ulivyowaongoza watu wako, nawe ukajipatia jina tukufu.” Ututazame kutoka mbinguni ee Mungu, uone, utuangalie kutoka makao yako matakatifu na matukufu. Iko wapi bidii yako kwa ajili yetu na nguvu yako? Usiache kutuonesha upendo wako. Maana wewe ndiwe Baba yetu; Abrahamu, mzee wetu, hatujali, naye Israeli hatutambui; lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ni Baba yetu. Wewe umeitwa tangu kale: “Mkombozi wetu.” Ee Mwenyezi-Mungu, mbona unatukosesha njia zako? Mbona unatufanya kuwa wakaidi hata tusikuogope? Rudi ee Mungu kwa ajili ya watumishi wako, makabila ambayo daima yalikuwa mali yako. Kwa kitambo tu sisi watakatifu wako tulimiliki nchi, lakini maadui zetu wakaja wakaharibu maskani yako. Tumekuwa kama watu ambao hujawatawala kamwe, kama watu ambao hawakujulikana kwa jina lako. Laiti ungalizipasua mbingu ukashuka chini, milima ikakuona na kutetemeka kwa hofu! Ingeteketea kama moto uchomavyo kichaka, kama vile moto uchemshavyo maji. Njoo upate kuwajulisha maadui zako jina lako nayo mataifa yatetemeke kwa kuwako kwako! Wakati ulipotenda maajabu ambayo hatukutazamia, ulishuka chini nayo milima ikatetemeka ilipokuona. Tangu kale hakuna aliyepata kuona wala kusikia kwa masikio yake; hakuna aliyepata kumwona Mungu aliye kama wewe atendaye mambo kwa ajili ya wale wanaomtegemea! Wewe waja kuwasaidia watendao haki kwa furaha, wanaokukumbuka na kuzingatia njia zako. Ulitukasirikia tulipokuwa wenye dhambi; sisi tumeasi kwa muda mrefu. Sote tumekuwa kama watu walio najisi; matendo yetu yote mema ni kama nguo chafu. Sote tunanyauka kama majani, uovu wetu watupeperusha kama upepo. Hakuna hata mmoja anayekuja kukuomba; hakuna anayejishughulisha kukutafuta. Wewe unauficha uso wako mbali nasi, umetuacha tukumbwe na maovu yetu. Hata hivyo, ee Mwenyezi-Mungu, wewe ni Baba yetu. Sisi ni kama udongo, wewe ni mfinyanzi. Sisi sote ni kazi ya mikono yako. Usitukasirikie mno, ee Mwenyezi-Mungu, usiukumbuke uovu wetu daima! Ukumbuke kwamba sisi sote ni watu wako! Miji yako mitakatifu imekuwa nyika; Siyoni umekuwa mahame, Yerusalemu umekuwa uharibifu. Nyumba yetu takatifu na nzuri, ambamo wazee wetu walikusifu, imeteketezwa kwa moto. Mahali petu pote pazuri pamekuwa magofu. Je, kwa hayo yote utajizuia usifanye kitu? Je, utaendelea kunyamaza tu, ee Mwenyezi-Mungu, na kututesa kupita kiasi? Mwenyezi-Mungu asema; “Nilikuwa tayari kujionesha kwao wasiouliza habari zangu. Nilikuwa tayari kuwapokea wale wasionitafuta. Nililiambia taifa ambalo halikuomba kwa jina langu: ‘Nipo hapa! Nipo hapa!’ Mchana kutwa niliwanyoshea mikono watu waasi, watu ambao hufuata njia zisizo sawa, watu ambao hufuata fikira zao wenyewe. Ni watu ambao daima hunichokoza waziwazi; hutambikia miungu yao katika bustani, na kuifukizia ubani juu ya matofali. Huketi makaburini na kukaa mafichoni usiku. Hula nyama ya nguruwe na mchuzi wa wanyama haramu. Huwaambia wale wanaokutana nao: ‘Kaeni mbali nami; msinikaribie kwani mimi ni mtakatifu!’ Watu hao wananikasirisha mno, hasira yangu ni kama moto usiozimika. “Jueni kuwa nimelitia jambo hilo moyoni, sitanyamaza bali nitawafanya walipe; nitawafanya walipe kwa wingi. Mimi Mwenyezi-Mungu, nitawalipiza maovu yao wayalipie na maovu ya wazee wao. Wao waliifukizia ubani miungu yao milimani, wakanitukana mimi huko vilimani. Nitawafanya walipe kwa wingi, watayalipia matendo yao ya awali.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mtu akikuta kishada cha zabibu nzuri, watu husema: ‘Tusikiharibu; kina baraka.’ Ndivyo nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu; sitawaangamiza wote. Nitawajalia watu wa Yakobo, na Yuda nitamjalia warithi wa milima yangu; watumishi wangu watakaa huko. Nchi tambarare ya Sharoni itakuwa malisho, bonde la Akori litakuwa mapumziko ya mifugo kwa ajili ya watu wangu walionitafuta. “Lakini nitafanya nini na nyinyi mnaoniacha mimi Mwenyezi-Mungu, msioujali Siyoni, mlima wangu mtakatifu, nyinyi mnaoabudu mungu ‘Gadi’, na kumtolea tambiko ya divai mungu ‘Meni’? Nimewapangia kifo kwa upanga, nyote mtaangukia machinjoni! Maana, nilipowaita, hamkuniitikia; niliponena, hamkunisikiliza. Mlitenda yaliyo maovu mbele yangu, mkachagua yale nisiyoyapenda. Basi, mimi Mwenyezi-Mungu nasema, watumishi wangu watakula, lakini nyinyi mtaona njaa; watumishi wangu watakunywa, lakini nyinyi mtaona kiu; watumishi wangu watafurahi, lakini nyinyi mtafedheheka. Watumishi wangu wataimba kwa furaha moyoni, lakini nyinyi mtalia kwa uchungu moyoni na kupiga kelele kwa uchungu mkubwa rohoni. Wale niliowachagua nitawapa jina jipya. Lakini nyinyi jina lenu watalitumia kulaania; ‘Watasema: Bwana Mungu awaue kama hao.’ Basi, mwenye kujitakia baraka nchini, atajitakia baraka kwa Mungu wa kweli. Mwenye kuapa katika nchi hii, ataapa kwa Mungu wa kweli. Maana taabu za zamani zimepita zimetoweka kabisa mbele yangu. “Sasa, naumba mbingu mpya na dunia mpya. mambo ya zamani hayatakumbukwa tena. Furahini, mkashangilie milele, kwa ajili ya vitu hivi ninavyoumba. Yerusalemu nitaufanya mji wa shangwe, na watu wake watu wenye furaha. Nami nitaufurahia mji wa Yerusalemu, nitawafurahia watu wangu. Sauti ya kilio haitasikika tena, kilio cha taabu hakitakuwako. Hakutakuwa tena na vifo vya watoto wachanga, wazee nao hawatakufa kabla ya wakati wao. Akifa mtu wa miaka 100 amekufa akiwa kijana; na akifa kabla ya miaka 100 ni balaa. Watu watajenga nyumba na kuishi humo; watalima mizabibu na kula matunda yake. Hawatajenga nyumba zikaliwe na watu wengine, wala kulima chakula kiliwe na watu wengine. Maana watu wangu niliowachagua wataishi maisha marefu kama miti; wateule wangu watafurahia matunda ya jasho lao. Kazi zao hazitakuwa bure, wala hawatazaa watoto wa kupata maafa; maana watakuwa waliobarikiwa na Mwenyezi-Mungu, wamebarikiwa wao pamoja na wazawa wao. Hata kabla hawajaniita, mimi nitawaitikia; kabla hawajamaliza kusema, nitakuwa nimewajibu. Mbwamwitu na kondoo watakula pamoja, simba watakula nyasi kama ng'ombe, nao nyoka chakula chao kitakuwa vumbi. Katika mlima wangu wote mtakatifu, hakuna atakayeumiza au kuharibu kitu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mbingu ni kiti changu cha enzi, dunia ni kiti cha kuwekea miguu yangu. Mtanijengea nyumba ya namna gani basi, Mahali nitakapoweza kupumzika? Mimi mwenyewe nilivifanya vitu hivi vyote, na hivi vyote ni mali yangu. Lakini ninachojali mimi ni mtu mnyenyekevu na mwenye majuto, mtu anayetetemeka asikiapo neno langu. “Lakini watu hawa wanafanya wanavyotaka: Wananitolea tambiko ya ng'ombe na mara wanaua watu kutambikia. Wananitolea sadaka ya mwanakondoo na pia wanamvunja mbwa shingo. Wananitolea tambiko ya nafaka na pia kupeleka damu ya nguruwe. Wanachoma ubani mbele yangu na kwenda kuabudu miungu ya uongo. Hao wamechagua kufuata njia zao wenyewe. Basi, nitawaletea taabu; yatawapata yaleyale wanayoyahofia; maana nilipoita hakuna aliyeitika, niliponena hawakusikiliza. Bali walifanya yaliyo maovu mbele yangu, walichagua yale ambayo hayanipendezi.” Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi msikiao neno lake mkatetemeka: “Ndugu zenu ambao wanawachukia, na kuwapiga marufuku kwa sababu yangu, wamesema kwa dharau ‘Mungu na aoneshe utukufu wake, nasi tuwaone nyinyi mkishinda!’ Lakini wao wenyewe ndio watakaoaibishwa! Sikilizeni, ghasia kutoka mjini, sauti kutoka hekaluni! Hiyo ni sauti ya Mwenyezi-Mungu akiwaadhibu maadui zake! “Mji wangu mtakatifu, ni kama mama ajifunguaye bila kuona uchungu; kabla uchungu kuanza, amekwisha zaa mtoto. Ni nani aliyepata kusikia jambo kama hilo? Ni nani aliyewahi kuona jambo kama hilo? Je, nchi nzima yaweza kuzaliwa siku moja? Je, taifa zima laweza kuzaliwa mara moja? Maana Siyoni, mara tu alipoanza kuona uchungu, alijifungua watoto wake. Je, nitawatunza watu wangu mpaka karibu wazaliwe, halafu niwazuie wasizaliwe? Au mimi mwenye kuwajalia watoto, nitafunga kizazi chao? Mimi Mungu wenu nimesema.” Shangilieni na kufurahi pamoja na Yerusalemu enyi mnaoupenda! Shangilieni pamoja nao enyi nyote mlioulilia! Kama mama, Yerusalemu utawanyonyesha, nanyi mtashiba kwa riziki zake; mtakunywa shibe yenu na kufurahi, kutokana na wingi wa fahari yake. Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nitakuletea fanaka nyingi kama mto, utajiri wa mataifa kama mto uliofurika. Nanyi mtanyonya na kubebwa kama mtoto mchanga, mtabembelezwa kama mtoto magotini mwa mama yake. Kama mama amtulizavyo mwanawe, kadhalika nami nitawatuliza; mtatulizwa mjini Yerusalemu. Mtayaona hayo na mioyo yenu itafurahi; mifupa yenu itapata nguvu kama majani mabichi. Hapo itajulikana kuwa mimi Mwenyezi-Mungu huwalinda watumishi wangu, lakini nikikasirika huwaadhibu maadui zangu.” Mwenyezi-Mungu atakuja kama moto, na magari yake ya vita ni kimbunga. Ataiacha hasira yake ifanye kazi yake kwa ukali, na onyo lake litekelezwe kwa miali ya moto. Mwenyezi-Mungu atatoa hukumu kwa moto, atawaadhibu watu wote kwa upanga; nao atakaowaangamiza watakuwa wengi. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wapo watu wanaojitakasa na kutawadha wapate kuingia kwenye bustani za ibada za sanamu; wanafanya maandamano na kuhani akiwa kati yao. Watu hao hula nguruwe, panya na vyakula vingine haramu. Watu hao hakika watakufa wote pamoja. Nayajua matendo yao na mawazo yao. Naja kuwakusanya watu wa mataifa yote na lugha zote, wajumuike pamoja na kuuona utukufu wangu. Nitaweka kati yao alama ya uwezo wangu. Watakaosalimika kati yao nitawapeleka kwa watu wa mataifa huko Tarshishi, Puti, Ludi, nchi zenye wapiga upinde stadi; watakwenda pia Tubali na Yowani na nchi ambapo watu hawajapata kusikia umaarufu wangu wala kuuona utukufu wangu. Hao wajumbe wangu watautangaza utukufu wangu katika mataifa hayo. Watawarejesha ndugu zenu wote kutoka katika mataifa yote kama matoleo yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Watawaleta wamepanda farasi, nyumbu, ngamia na magari ya farasi mpaka Yerusalemu, kwenye mlima wangu mtakatifu. Watawaleta kama Waisraeli waletavyo sadaka ya nafaka katika chombo safi hadi nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu. Pia nitawachagua baadhi yao kuwa makuhani na baadhi yao kuwa Walawi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Kama vile mbingu mpya na dunia mpya nitakazoumba zitakavyodumu milele kwa uwezo wangu, ndivyo wazawa wako na jina lako litakavyodumu. Katika kila sikukuu ya mwezi mpya, na katika kila siku ya Sabato, binadamu wote watakuja kuniabudu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Kisha watakwenda kuziona maiti za wale walioniasi. Wadudu watakaowala hawatakufa, na moto utakaowachoma hautazimika kamwe. Watakuwa chukizo kwa watu wote.” Yafuatayo ni maneno ya Yeremia mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani wa mji wa Anathothi, katika nchi ya Benyamini. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia mnamo mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda. Lilimjia tena wakati Yehoyakimu mwana wa Yosia, alipokuwa mfalme wa Yuda. Yeremia aliendelea kupata neno la Mwenyezi-Mungu hadi mwishoni mwa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda. Mnamo mwezi wa tano wa mwaka huo, watu wa Yerusalemu walipelekwa uhamishoni. Mwenyezi-Mungu aliniambia neno lake: “Kabla hujachukuliwa mimba, mimi nilikujua, kabla hujazaliwa, mimi nilikuweka wakfu; nilikuteua uwe nabii kwa mataifa.” Nami nikajibu, Aa! Bwana Mwenyezi-Mungu, mimi sijui kusema, kwa kuwa bado ningali kijana. Lakini Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Usiseme kwamba wewe ni kijana bado. Utakwenda kwa watu wote nitakaokutuma kwao, na yote nitakayokuamuru utayasema. Wewe usiwaogope watu hao, kwa maana niko pamoja nawe kukulinda. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Kisha Mwenyezi-Mungu akaunyosha mkono wake, akagusa kinywa changu, akaniambia, “Tazama nimeyatia maneno yangu kinywani mwako. Leo nimekupa mamlaka juu ya mataifa na falme, uwe na mamlaka ya kungoa na kubomoa, mamlaka ya kuharibu na kuangamiza, mamlaka ya kujenga na ya kupanda.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Yeremia, unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona tawi la mlozi unaochanua.” Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Umeona vizuri, maana niko macho kulitekeleza neno langu.” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili: “Unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona chungu kinatokota kimeinama upande wangu kutoka kaskazini.” Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Maangamizi yataanzia kutoka kaskazini na kuwapata wakazi wote wa nchi hii. Maana naziita falme zote za kaskazini na makabila yote. Wafalme wake wote watakuja na kila mmoja wao ataweka kiti chake cha enzi mbele ya malango ya Yerusalemu na kandokando ya kuta zake zote, na kuizunguka miji yote ya Yuda. Nami nitawahukumu Waisraeli kwa ajili ya uovu wao wote wa kuniacha mimi, wakafukizia ubani miungu mingine na kuabudu sanamu walizojitengenezea wenyewe. Sasa basi, wewe Yeremia jiweke tayari. Haya! Nenda ukawaambie mambo yote ninayokuamuru. Usiwaogope, nisije nikakufanya mwoga mbele yao. Leo hii nakufanya kuwa imara kama mji uliozungukwa na ngome, kama mnara wa chuma na kama ukuta wa shaba nyeusi, dhidi ya nchi yote, dhidi ya wafalme wa Yuda, wakuu wake, makuhani wake na watu wake wote. Watapigana nawe, lakini hawatashinda kwa sababu mimi niko pamoja nawe kukuokoa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Nenda ukawatangazie waziwazi wakazi wote wa Yerusalemu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Naukumbuka uaminifu wako ulipokuwa kijana, jinsi ulivyonipenda kama mchumba wako, ulivyonifuata jangwani kwenye nchi ambayo haikupandwa kitu. Israeli, wewe ulikuwa mtakatifu kwangu, ulikuwa matunda ya kwanza ya mavuno yangu. Wote waliokudhuru walikuwa na hatia, wakapatwa na maafa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi wazawa wa Yakobo. Sikilizeni enyi jamaa zote za wazawa wa Israeli. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wazee wenu waliona kosa gani kwangu hata wakanigeuka na kuniacha, wakakimbilia miungu duni, hata nao wakawa watu duni? Hawakujiuliza: ‘Yuko wapi Mwenyezi-Mungu aliyetutoa nchini Misri, aliyetuongoza nyikani katika nchi ya jangwa na makorongo, nchi kame na yenye giza nene, nchi isiyopitiwa na mtu yeyote, wala kukaliwa na binadamu?’ Niliwaleta katika nchi yenye rutuba, muyafurahie mazao yake na mema yake mengine. Lakini mlipofika tu mliichafua nchi yangu, mkaifanya chukizo nchi niliyowapa iwe yenu. Nao makuhani hawakujiuliza: ‘Yuko wapi Mwenyezi-Mungu?’ Wataalamu wa sheria hawakunijua, viongozi wa watu waliniasi; manabii nao walitabiri kwa jina la Baali na kuabudu sanamu zisizo na faida yoyote.” Mwenyezi-Mungu asema, “Kwa hiyo, mimi nitawalaumu nyinyi, na nitawalaumu wazawa wenu. Haya, vukeni bahari hadi Kupro mkaone, au tumeni watu huko Kedari wakachunguze, kama jambo kama hili limewahi kutokea: Kwamba kuna taifa lililowahi kubadilisha miungu yake ingawa miungu hiyo si miungu! Lakini watu wangu wameniacha mimi, utukufu wao, wakafuata miungu isiyofaa kitu. Shangaeni enyi mbingu, juu ya jambo hili, mkastaajabu na kufadhaika kabisa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Maana, watu wangu wametenda maovu mawili; wameniacha mimi niliye chemchemi ya maji ya uhai, wakajichimbia visima vyao wenyewe, visima vyenye nyufa, visivyoweza kuhifadhi maji. “Je, Israeli ni mtumwa, ama amezaliwa utumwani? Mbona basi amekuwa kama mawindo? Simba wanamngurumia, wananguruma kwa sauti kubwa. Nchi yake wameifanya jangwa, miji yake imekuwa magofu, haina watu. Isitoshe, watu wa Memfisi na Tahpanesi, wameuvunja utosi wake. Israeli, je, hayo yote si umejiletea mwenyewe, kwa kuniacha mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekuwa ninakuongoza njiani? Na sasa itakufaa nini kwenda Misri, kunywa maji ya mto Nili? Au itakufaa nini kwenda Ashuru, kunywa maji ya mto Eufrate? Uovu wako utakuadhibu; na uasi wako utakuhukumu. Ujue na kutambua kuwa ni vibaya mno kuniacha mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na kuondoa uchaji wangu ndani yako. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. “Tangu zamani wewe ulivunja nira yako, ukaikatilia mbali minyororo yako, ukasema, ‘Sitakutumikia’. Juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wa majani mabichi, uliinamia miungu ya rutuba kama kahaba. Lakini mimi nilikupanda kama mzabibu mteule, mzabibu wenye afya na wa mbegu safi; mbona basi umeharibika, ukageuka kuwa mzabibu mwitu? Hata ukijiosha kwa magadi, na kutumia sabuni nyingi, madoa ya uovu wako bado yatabaki mbele yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Unawezaje kusema, ‘Mimi si najisi; sijawafuata Mabaali?’ Tazama ulivyotenda dhambi kule bondeni; angalia ulivyofanya huko! Wewe ni kama mtamba wa ngamia, akimbiaye huko na huko; kama pundamwitu aliyezoea jangwani. Katika tamaa yake hunusanusa upepo; nani awezaye kuizuia hamu yake? Amtakaye hana haja ya kujisumbua; wakati wake ufikapo watampata tu. Israeli, usiichakaze miguu yako wala usilikaushe koo lako. Lakini wewe wasema: ‘Hakuna tumaini lolote. Nimeipenda miungu ya kigeni, hiyo ndiyo nitakayoifuata.’ “Kama vile mwizi aonavyo aibu akishikwa, ndivyo Waisraeli watakavyoona aibu; wao wenyewe, wafalme wao, wakuu wao, makuhani wao na manabii wao. Hao huuambia mti: ‘Wewe u baba yangu,’ na jiwe: ‘Wewe ndiwe uliyenizaa;’ kwa maana wamenipa kisogo, wala hawakunielekezea nyuso zao. Lakini wakati wa shida husema: ‘Inuka utuokoe!’ “Lakini iko wapi miungu yako uliyojifanyia? Iinuke basi, kama inaweza kukusaidia, wakati unapokuwa katika shida. Ee Yuda, idadi ya miungu yako ni sawa na idadi ya miji yako! Mbona mnanilalamikia? Nyinyi nyote mmeniasi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Niliwaadhibu watu wako bila kufanikiwa, wao wenyewe walikataa kukosolewa. Upanga wako uliwamaliza manabii wako kama simba mwenye uchu. Enyi watu! Sikilizeni ninachosema mimi Mwenyezi-Mungu: Je, nimekuwa jangwa kwa Israeli au nchi yenye giza nene? Kwa nini basi watu wangu waseme: ‘Sisi tu watu huru; hatutakuja kwako tena!’ Kijana msichana aweza kusahau mapambo yake au bibi arusi mavazi yake? Lakini watu wangu wamenisahau kwa muda wa siku zisizohesabika. Kweli wewe ni bingwa wa kutafuta wapenzi! Hata wanawake wabaya huwafundisha njia zako. Nguo zako zina damu ya maskini wasio na hatia, japo hukuwakuta wakivunja nyumba yako. “Lakini licha ya hayo yote, wewe wasema: ‘Mimi sina hatia; hakika hasira yake imegeuka mbali nami.’ Lakini mimi nitakuhukumu kwa sababu unasema: ‘Sikutenda dhambi.’ Kwa nini unajirahisisha hivi, ukibadilibadili mwenendo wako? Utaaibishwa na Misri, kama ulivyoaibishwa na Ashuru. Na huko pia utatoka, mikono kichwani kwa aibu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa wale uliowategemea, wala hutafanikiwa kwa msaada wao. “Mume akimpa talaka mkewe, naye akaondoka kwake, na kuwa mke wa mwanamume mwingine, je mume yule aweza kumrudia mwanamke huyo? Je, kufanya hivyo hakutaitia nchi unajisi mkubwa? Wewe Israeli, umefanya ukahaba na wapenzi wengi, je, sasa unataka kunirudia mimi? Inua macho uvitazame vilele vya vilima! Pako wapi mahali ambapo hawajalala nawe? Uliwangoja wapenzi wako kando ya njia, kama bedui aviziavyo watu jangwani. Umeifanya nchi kuwa najisi, kwa ukahaba wako mbaya kupindukia. Ndiyo maana manyunyu yamezuiliwa, na wala mvua za vuli hazijanyesha. Hata hivyo uko macho makavu kama kahaba, huna haya hata kidogo. “Hivi punde tu si ulinililia ukisema: ‘Wewe u baba yangu, ulinipenda tangu utoto wangu? Je, utanikasirikia daima? Utachukizwa nami milele?’ Israeli, hivyo ndivyo unavyosema; na kumbe umetenda uovu wote ulioweza.” Wakati wa utawala wa mfalme Yosia, Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Je, umeona jinsi Israeli asiye mwaminifu alivyofanya? Aliniacha, akapanda juu ya kila kilima kirefu na kwenda chini ya kila mti wenye majani mabichi, akafanya ukahaba wake humo! Mimi nilidhani kuwa baada ya kufanya yote hayo, atanirudia. Lakini wapi; hakunirudia. Yuda, dada yake mdanganyifu, alishuhudia yote hayo. Zaidi ya hayo, Yuda alishuhudia kuwa nilimpa Israeli talaka kwa sababu ya ukahaba wake na kwa kukosa uaminifu kwangu. Lakini hata hivyo, Yuda, dada yake mdanganyifu, hakuogopa; naye pia alikwenda na kufanya ukahaba! Na, kwa kuwa yeye aliona kuwa ukahaba ni jambo dogo sana kwake, aliitia nchi unajisi, na kufanya ukahaba kwa kuabudu mawe na miti. Pamoja na hayo yote, Yuda, dada mdanganyifu wa Israeli, hakunirudia kwa moyo wote, bali kwa unafiki tu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Mwasi Israeli amedhihirisha kuwa yeye ni afadhali kuliko Yuda mdanganyifu. Basi, nenda ukamtangazie Israeli maneno yafuatayo: Rudi, ewe Israeli, usiye mwaminifu. Nami sitakutazama kwa hasira kwa kuwa mimi ni mwenye huruma. Naam, sitakukasirikia milele. Wewe, kiri tu kosa lako: Kwamba umeniasi mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; kwamba chini ya kila mti wenye majani, umewapa miungu wengine mapenzi yako wala hukuitii sauti yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Rudini, enyi watoto msio na uaminifu, maana, mimi ndimi Bwana wenu. Nitawachukua mmoja kutoka kila mji, na wawili kutoka katika kila ukoo, niwapeleke hadi mlimani Siyoni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitawapeni wachungaji wanipendao moyoni, watakaowalisha kwa maarifa na busara. Siku hizo, wakati mtakapokuwa mmeongezeka na kuwa wengi nchini, watu hawatalitajataja tena sanduku langu la agano. Hawatalifikiria kabisa, wala hawatalikumbuka tena; hawatalihitaji, wala hawataunda jingine. Wakati huo, mji wa Yerusalemu utaitwa ‘Kiti cha Enzi cha Mwenyezi-Mungu’, na mataifa yote yatakusanyika humo mbele yangu. Hawatafuata tena ukaidi wa matendo yao. Siku hizo, watu wa Yuda wataungana na watu wa Israeli, na wote kwa pamoja watatoka katika nchi ya kaskazini na kurudi katika nchi niliyowapa wazee wenu iwe mali yao.” Mwenyezi-Mungu asema, “Israeli, mimi niliwaza, laiti ningekuweka miongoni mwa wanangu, na kukupa nchi nzuri ajabu, urithi usio na kifani kati ya mataifa yote. Nilidhani ungeniita, ‘Baba Yangu’, na kamwe usingeacha kunifuata. Lakini kama mke asiye mwaminifu amwachavyo mumewe, ndivyo ulivyokosa uaminifu kwangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Kelele zasikika juu ya vilima: Waisraeli wanalia na kuomboleza, kwa kuwa wamepotoka katika njia zao, wamenisahau mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Rudini, enyi watoto msio na uaminifu, mimi nitaponya utovu wenu wa uaminifu. “Nanyi mwasema: ‘Tazama, sisi tunarudi kwako, maana, wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Kweli tumedanganyika mno kuabudu huko vilimani, hakika wokovu wa Israeli watoka kwake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. “ ‘Tangu ujana wetu, tendo hili la aibu limeangamiza kila kitu walichotolea jasho wazee wetu: Makundi yao ya kondoo na ng'ombe, wana wao na binti zao. Hatuna budi kujilaza chini kwa aibu, na kuiacha fedheha yetu itufunike. Tangu ujana wetu hadi leo hii, wazee wetu na sisi wenyewe tumetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala hatukumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ukitaka kurudi ee Israeli, nirudie mimi. Ukiviondoa vitu vya kuchukiza mbele yangu, usipotangatanga huko na huko, ukiapa kwa ukweli, unyofu na uadilifu, kwa kusema, ‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo’, ndipo mataifa yatakapopata baraka kwangu, na kutukuka kwa sababu yangu.” Mwenyezi-Mungu awaambia hivi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu: “Limeni mashamba yenu mapya; msipande mbegu zenu penye miiba. Enyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, jitakaseni kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu, wekeni mioyo yenu wazi mbele yangu. La sivyo, ghadhabu yangu itachomoza kama moto, iwake hata pasiwe na mtu wa kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu. “Tangazeni huko Yuda, pazeni sauti huko Yerusalemu! Pigeni tarumbeta kila mahali nchini! Pazeni sauti na kusema: Kusanyikeni pamoja! Kimbilieni miji yenye ngome! Twekeni bendera ya vita kuelekea Siyoni, kimbilieni usalama wenu, msisitesite! Mwenyezi-Mungu analeta maafa na maangamizi makubwa kutoka kaskazini. Kama simba atokavyo mafichoni mwake, mwangamizi wa mataifa ameanza kuja, anakuja kutoka mahali pake, ili kuiharibu nchi yako. Miji yako itakuwa magofu matupu, bila kukaliwa na mtu yeyote. Kwa hiyo, vaa vazi la gunia, omboleza na kulia; maana, hasira kali ya Mwenyezi-Mungu, bado haijaondoka kwetu. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Siku hiyo, mfalme na wakuu watakufa moyo; makuhani watapigwa na bumbuazi, na manabii watashangaa.” Kisha nikasema: “Aa, Mwenyezi-Mungu, hakika umewadanganya kabisa watu hawa na mji wa Yerusalemu! Uliwaambia mambo yatawaendea vema, kumbe maisha yao yamo hatarini kabisa!” Wakati huo, wataambiwa hivi watu hawa pamoja na mji wa Yerusalemu, “Upepo wa hari kutoka vilele vikavu vya jangwani utawavumia watu wangu. Huo si upepo wa kupepeta au kusafisha, bali ni upepo mkali sana utokao kwangu. Ni mimi Mwenyezi-Mungu nitakayetoa hukumu juu yao.” Tazama! Adui anakuja kama mawingu. Magari yake ya vita ni kama kimbunga, na farasi wake waenda kasi kuliko tai. Ole wetu! Tumeangamia! Yerusalemu, yasafishe maovu moyoni mwako, ili upate kuokolewa. Mpaka lini utaendelea kuwaza maovu? Sauti kutoka Dani inatoa taarifa; inatangaza maafa kutoka vilima vya Efraimu. Inayaonya mataifa, inaitangazia Yerusalemu: “Wavamizi waja kutoka nchi ya mbali, wanaitisha miji ya Yuda, wanauzingira Yerusalemu kama walinda mashamba, kwa sababu watu wake wameniasi mimi Mwenyezi-Mungu. Yuda, mwenendo wako na matendo yako yamekuletea hayo. Hayo ndiyo maafa yaliyokupata, tena ni machungu; yamepenya mpaka ndani moyoni mwako.” Uchungu, uchungu! Nagaagaa kwa uchungu! Moyo wangu unanigonga vibaya. Wala siwezi kukaa kimya. Maana naogopa mlio wa tarumbeta, nasikia kingora cha vita. Maafa baada ya maafa, nchi yote imeharibiwa. Ghafla makazi yangu yameharibiwa, na hata mapazia yake kwa dakika moja. Hadi lini nitaona bendera ya vita na kuisikia sauti ya tarumbeta? Mwenyezi-Mungu asema: “Watu wangu ni wapumbavu, hawanijui mimi. Wao ni watoto wajinga; hawaelewi kitu chochote. Ni mabingwa sana wa kutenda maovu, wala hawajui kutenda mema.” Niliiangalia nchi, lo! Imekuwa mahame na tupu; nilizitazama mbingu, nazo hazikuwa na mwanga. Niliiangalia milima, lo, ilikuwa inatetemeka, na vilima vyote vilikuwa vinayumbayumba. Nilikodoa macho wala sikuona mtu; hata ndege angani walikuwa wametoweka. Niliona nchi yenye rutuba imekuwa jangwa, na miji yake yote imekuwa magofu matupu, kwa sababu ya hasira kali ya Mwenyezi-Mungu. Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nchi nzima itakuwa jangwa tupu; lakini sitaiharibu kabisa. Kwa hiyo, nchi itaomboleza, na mbingu zitakuwa nyeusi. Maana, nimetamka na sitabadili nia yangu; nimeamua, wala sitarudi nyuma. Watakaposikika wapandafarasi na wapiga mishale, kila mmoja atatimua mbio. Baadhi yao watakimbilia msituni, wengine watapanda majabali. Kila mji utaachwa tupu; hakuna mtu atakayekaa ndani. Nawe Yerusalemu uliyeachwa tupu, unavalia nini mavazi mekundu? Ya nini kujipamba kwa dhahabu, na kujipaka wanja machoni? Unajirembesha bure! Wapenzi wako wanakudharau sana; wanachotafuta ni kukuua. Nilisikia sauti kama ya mwanamke anayejifungua, yowe kama anayejifungua mtoto wa kwanza. Ilikuwa sauti ya Yerusalemu akitweta, na kuinyosha mikono yake akisema, ‘Ole wangu! Wanakuja kuniua!’” Kimbieni huko na huko mjini Yerusalemu; pelelezeni na kujionea wenyewe! Chunguzeni masoko yake mwone kama kuna mtu atendaye haki mtu atafutaye ukweli; akiwako, basi Mwenyezi-Mungu atausamehe Yerusalemu. Ingawa wanaapa: “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo”, viapo vyao ni vya uongo. Ee Mwenyezi-Mungu, wewe watafuta daima uaminifu. Umewatwanga, lakini hawakuona uchungu; umewateketeza, lakini walikataa kukosolewa. Wamezifanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko mwamba; wamekataa kabisa kurudi kwako. Ndipo nilipowaza: “Hawa ni watu duni hawana akili; hawajui matakwa ya Mwenyezi-Mungu, hawajui Sheria ya Mungu wao. Nitawaendea wakuu niongee nao; bila shaka, wao wanajua matakwa ya Mwenyezi-Mungu; wanajua sheria ya Mungu wao.” Lakini wote waliivunja nira yao. Waliikatilia mbali minyororo yao. Kwa hiyo simba kutoka msituni atawaua; mbwamwitu kutoka jangwani atawararua. Chui anaivizia miji yao. Kila atokaye humo atararuliwa vipandevipande, kwa sababu dhambi zao ni nyingi, maasi yao ni makubwa. Mwenyezi-Mungu anauliza: “Nitawezaje kukusamehe ee Yerusalemu? Watu wako wameniasi; wameapa kwa miungu ya uongo. Nilipowashibisha kwa chakula, wao walifanya uzinzi, wakajumuika majumbani mwa makahaba. Walikuwa kama farasi walioshiba wenye tamaa, kila mmoja akimtamani mke wa jirani yake. Je, nisiwaadhibu kwa mambo haya yote? Nisilipize kisasi juu ya taifa kama hili? “Pandeni mpite katika mashamba yake ya mizabibu mkaharibu kila kitu bila kumaliza kabisa. Yakateni matawi yake, kwani hayo si yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Naam, watu wa Israeli na watu wa Yuda, wamekosa kabisa uaminifu kwangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Wamesema uongo juu ya Mwenyezi-Mungu wamesema: “Hatafanya kitu; hatutapatwa na uovu wowote; hatutashambuliwa wala kuona njaa. Manabii si kitu, ni upepo tu; maana neno lake Mungu halimo ndani yao.” Basi hayo na yawapate wao wenyewe! Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Kwa kuwa wao wamesema jambo hilo, sasa nitayafanya maneno niliyokupa wewe Yeremia kuwa moto. Watu hawa watakuwa kuni, na moto huo utawateketeza. “Nami Mwenyezi-Mungu nasema juu yenu enyi Waisraeli: Mimi naleta taifa moja kutoka mbali, lije kuwashambulia. Taifa ambalo halishindiki, taifa ambalo ni la zamani, ambalo lugha yake hamuifahamu, wala hamwezi kuelewa wasemacho. Mishale yao husambaza kifo; wote ni mashujaa wa vita. Watayala mazao yenu na chakula chenu; watawamaliza watoto wenu wa kike na wa kiume. Watachinja makundi yenu ya kondoo na ng'ombe; wataiharibu mizabibu yenu na mitini yenu. Miji yenu ya ngome mnayoitegemea, wataiharibu kwa silaha zao. “Lakini, hata katika siku hizo mimi Mwenyezi-Mungu nasema, sitawaangamiza na kuwamaliza kabisa. Na watu wenu watakapouliza ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametutendea mambo hayo yote?’ Wewe utawaambia, ‘Nyinyi mlimwacha Mwenyezi-Mungu, mkaitumikia miungu ya kigeni katika nchi yenu. Basi ndivyo mtakavyowatumikia watu wengine katika nchi isiyo yenu.’ “Watangazie wazawa wa Yakobo, waambie watu wa Yuda hivi: Sikilizeni enyi wajinga na wapumbavu; watu mlio na macho, lakini hamwoni, mlio na masikio, lakini hamsikii. Mbona hamniogopi? Nauliza mimi Mwenyezi-Mungu! Kwa nini hamtetemeki mbele yangu? Mimi niliweka mchanga uwe mpaka wa bahari, kizuizi cha daima ambacho bahari haiwezi kuvuka. Ingawa mawimbi yanaupiga, hayawezi kuupita; ingawa yananguruma, hayawezi kuuruka. Lakini watu hawa wana moyo wa ukaidi na uasi; wameniacha wakaenda zao. Wala hawasemi mioyoni mwao; ‘Na tumche Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, anayetujalia mvua kwa wakati wake, anayetupatia mvua za masika na mvua za vuli; na kutupa majira maalumu ya mavuno.’ Makosa yenu yamewazuia msipate baraka hizo, dhambi zenu zimewafanya msipate mema. Naam, kuna walaghai miongoni mwa watu wangu, watu ambao hunyakua mali za wengine. Wako kama wawindaji wa ndege: Hutega mitego yao na kuwanasa watu. Kama vile kapu lililojaa ndege walionaswa, ndivyo nyumba zao zilivyojaa mali za udanganyifu. Ndiyo maana wamekuwa watu wakubwa na matajiri, wamenenepa na kunawiri. Katika kutenda maovu hawana kikomo hawahukumu yatima kwa haki wapate kufanikiwa, wala hawatetei haki za watu maskini. “Je, nisiwaadhibu kwa mambo haya? Je nitaacha kulipiza kisasi taifa kama hili? Jambo la ajabu na la kuchukiza limetokea katika nchi hii: Manabii wanatabiri mambo ya uongo, makuhani nao hutafuta faida yao wenyewe; na watu wangu wanaona jambo hilo kuwa sawa. Lakini mwisho utakapofika mtafanyaje?” Enyi watu wa Benyamini, ondokeni Yerusalemu mkimbilie usalama! Pigeni tarumbeta mjini Tekoa; onesheni ishara huko Beth-hakeremu, maana maafa na maangamizi makubwa yanakuja kutoka upande wa kaskazini. Mji wa Siyoni ni mzuri na mwororo, lakini utaangamizwa. Watu wataujia kama wachungaji na makundi yao, watapiga hema zao kuuzunguka kila mmoja sehemu yake, wapate kuyaongoza makundi yao. Watasema: “Jitayarisheni kuushambulia Siyoni. Haya! Tuanze kushambulia adhuhuri! Bahati mbaya; jua linatua! Kivuli cha jioni kinarefuka. Basi, tutaushambulia usiku; tutayaharibu majumba yake ya kifalme.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Kateni miti yake, rundikeni udongo kuuzingira Yerusalemu. Mji huu ni lazima uadhibiwe, maana hamna lolote ndani yake ila dhuluma. Kama kisima kinavyohifadhi maji yake yakabaki safi, ndivyo Yerusalemu unavyohifadhi uovu wako. Ukatili na uharibifu vyasikika ndani yake, magonjwa na majeraha yake nayaona daima. Hilo na liwe onyo kwako ee Yerusalemu, la sivyo nitakutupa kabisa kwa chuki; nikakufanya uwe jangwa, mahali pasipokaliwa na mtu.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Kusanyeni watu wote wa Israeli waliobaki kama watu wakusanyavyo zabibu zote; kama afanyavyo mchumazabibu, pitisheni tena mikono yenu katika matawi yake.” Nitaongea na nani nipate kumwonya, ili wapate kunisikia? Tazama, masikio yao yameziba, hawawezi kusikia ujumbe wako. Kwao neno lako, ee Mwenyezi-Mungu, limekuwa jambo la dhihaka, hawalifurahii hata kidogo. Nimejaa hasira ya Mwenyezi-Mungu dhidi yao. Nashindwa kuizuia ndani yangu. Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Imwage hasira barabarani juu ya watoto na pia juu ya makundi ya vijana; wote, mume na mke watachukuliwa, kadhalika na wazee na wakongwe. Nyumba zao zitapewa watu wengine, kadhalika na mashamba yao na wake zao; maana nitaunyosha mkono wangu, kuwaadhibu wakazi wa nchi hii. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wote, tangu mdogo hadi mkubwa kabisa, kila mmoja anatamani kupata faida isiyo halali. Tangu manabii hadi makuhani, kila mmoja wao ni mdanganyifu. Wameliponya jeraha la watu wangu juujuu, wanasema; ‘Amani, amani’, kumbe hakuna amani yoyote! Je, waliona aibu walipofanya machukizo hayo? La! Hawakuona aibu hata kidogo. Hawakujua hata namna ya kuona aibu. Kwa hiyo wataanguka pamoja na wale waangukao; wakati nitakapowaadhibu, wataangamizwa kabisa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Simameni katika njia panda, mtazame. Ulizeni mjue juu ya matukio ya zamani. Tafuteni mahali ilipo njia nzuri muifuate nanyi mtapumzisha nafsi zenu. Lakini wao wakasema: ‘Hatutafuata njia hiyo.’ Kisha nikawawekea walinzi, nikawaambia: ‘Sikilizeni ishara ya tarumbeta.’ Lakini wao wakasema: ‘Hatutaisikiliza.’ “Kwa hiyo, sikilizeni enyi mataifa; enyi jumuiya ya watu jueni yatakayowapata. Sikiliza ee dunia! Mimi nitawaletea maafa watu hawa kulingana na nia zao mbaya. Maana hawakuyajali maneno yangu, na mafundisho yangu nayo wameyakataa. Ya nini kuniletea ubani kutoka Sheba, na udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali? Sadaka zenu za kuteketezwa hazikubaliki, wala tambiko zenu hazinipendezi. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tazama, nitawawekea watu hawa vikwazo ambavyo vitawakwaza na kuwaangusha chini. Akina baba na watoto wao wa kiume wataangamia, kadhalika na majirani na marafiki.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Tazameni, watu wanakuja toka nchi ya kaskazini; taifa kubwa linajitayarisha kutoka mbali duniani. Wamezishika pinde zao na mikuki, watu wakatili wasio na huruma. Vishindo vyao ni kama ngurumo ya bahari. Wamepanda farasi, wamejipanga tayari kwa vita, dhidi yako ewe Siyoni!” Waisraeli wanasema, “Tumesikia habari zao, mikono yetu imelegea; tumeshikwa na dhiki na uchungu, kama mwanamke anayejifungua. Hatuwezi kwenda mashambani, wala kutembea barabarani; maadui wameshika silaha mikononi, vitisho vimejaa kila mahali.” Mwenyezi-Mungu asema, “Jivikeni mavazi ya gunia, enyi watu wangu na kugaagaa katika majivu. Ombolezeni kwa uchungu, kama mtu anayemwombolezea mwana wa pekee, maana mwangamizi atakuja, na kuwashambulia ghafla. Yeremia, wewe nimekuweka kuwa mchunguzi na mpimaji wa watu wangu, ili uchunguze na kuzijua njia zao. Wote ni waasi wakaidi, ni watu wanaopitapita wakisengenya wengine, wagumu kama shaba nyeusi au chuma; wote hutenda kwa ufisadi. Mifuo inafukuta kwa nguvu, risasi inayeyukia humohumo motoni; ni bure kuendelea kuwatakasa watu wangu, waovu hawawezi kuondolewa uchafu wao. Wataitwa ‘Takataka za fedha’, maana mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa.” Mwenyezi-Mungu alimwamuru Yeremia aende kusimama kwenye lango la hekalu lake Mwenyezi-Mungu na kutangaza ujumbe huu: “Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu enyi watu wa Yuda mnaoingia humu kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Rekebisheni mienendo yenu na matendo yenu, nami nitawaacha mwendelee kukaa mahali hapa. Msitumainie maneno haya ya uongo: ‘Hili ni hekalu la Mwenyezi-Mungu, hekalu la Mwenyezi-Mungu, naam hekalu la Mwenyezi-Mungu.’ “Ila kama mkibadili mienendo yenu na matendo yenu, mkitendeana haki kwa dhati; kama mkiacha kuwadhulumu wageni, yatima au wajane au kuwaua watu wasio na hatia katika nchi hii; kama mkiacha kuabudu miungu mingine na kujiangamiza wenyewe, basi mimi nitawaacha daima mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa wazee wenu tangu zamani. “Lakini kumbe, mnayaamini maneno ya uongo bure. Mnaiba, mnaua, mnafanya uzinzi, mnaapa uongo, mnamfukizia mungu Baali ubani na kuabudu miungu mingine ambayo hamjapata kuijua. Kisha, mnakuja na kusimama mbele yangu, katika hekalu hili linalojulikana kwa jina langu na kusema; ‘Tuko salama,’ huku mnaendelea kufanya mambo hayo yanayonichukiza. Je, hekalu hili linalojulikana kwa jina langu limekuwa pango la wanyanganyi? Jueni kuwa mimi nimeyaona yote mnayofanya! Nendeni mahali pangu kule Shilo, mahali nilipopachagua niabudiwe hapo awali, mkaone maangamizi niliyoyafanya huko kwa sababu ya uovu wa watu wangu, Israeli. Nyinyi mmefanya mambo hayo yote, na hata niliposema nanyi tena na tena hamkunisikiliza. Nilipowaiteni hamkuitika. Kwa hiyo, kama nilivyoutendea mji wa Shilo, ndivyo nitakavyolitendea hekalu hili linalojulikana kwa jina langu, hekalu ambalo nyinyi mnalitegemea; naam, mahali hapa ambapo niliwapa nyinyi na wazee wenu. Nitawafukuzeni mbali nami kama nilivyowatupilia mbali ndugu zenu, wazawa wote wa Efraimu. “Nawe, Yeremia, usiwaombee watu hawa, usinililie kwa ajili yao, usiwaombee dua wala usinisihi kwa ajili yao, maana sitakusikiliza. Je, wewe huoni mambo wanayofanya katika miji ya Yuda na katika mitaa ya Yerusalemu? Watoto huokota kuni, akina baba huwasha moto na akina mama hukanda unga ili waoke mikate kwa ajili ya mungu wa kike wanayemwita malkia wa mbinguni. Tena wanaimiminia miungu mingine tambiko ya divai ili kuniudhi. Lakini je, wanamwudhi nani? Mimi? Hata kidogo! Wanajiumiza wao wenyewe na kuchanganyikiwa! Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitaimwaga hasira yangu na ghadhabu yangu mahali hapa, juu ya wanadamu na wanyama, miti mashambani na mazao ya nchi. Itawaka na wala haitaweza kuzimwa.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Haya, ongezeni tambiko zenu za kuteketezwa juu ya sadaka zenu na kula nyama yake! Maana, siku nilipowatoa wazee wenu nchini Misri, sikuwaambia kitu wala kuwapa amri yoyote juu ya tambiko za kuteketezwa na sadaka. Lakini niliwapa amri hii: Waitii sauti yangu ili niwe Mungu wao, nao wawe watu wangu. Niliwaamuru pia waishi kama nilivyowaagiza, ili mambo yao yawaendee vema. Lakini wao hawakunitii wala kunitegea sikio. Badala yake wakafuata fikira zao wenyewe na ukaidi wa mioyo yao, wakarudi nyuma badala ya kusonga mbele. Tangu siku ile wazee wenu walipotoka nchini Misri hadi leo, sijakoma kuwatuma kwenu watumishi wangu, manabii. Lakini hamkunisikiliza wala kunitegea sikio, ila mlizidi kuwa wakaidi, mkawa waasi kuliko hata wazee wenu. “Basi, wewe Yeremia utawaambia maneno haya yote, lakini wao hawatakusikiliza. Utawaita, lakini hawatakuitikia. Utawaambia; ‘Nyinyi ni taifa ambalo halikutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, wala kukubali kuwa na nidhamu. Kwenu uaminifu umekufa; umetoweka kabisa katika maneno yenu.’ “Nyoeni nywele zenu enyi wakazi wa Yerusalemu, mzitupe; fanyeni maombolezo juu ya vilele vya milima, maana, mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa nyinyi, mlio kizazi kilichosababisha hasira yangu! “Watu wa Yuda wametenda uovu mbele yangu. Wameweka vinyago vyao vya kuchukiza ndani ya nyumba hii ijulikanayo kwa jina langu, wakaitia unajisi. Wamejenga madhabahu iitwayo ‘Tofethi’ huko kwenye bonde la mwana wa Hinomu, wapate kuwachoma sadaka watoto wao wa kiume na wa kike humo motoni. Mimi sikuwa nimewaamuru kamwe kufanya jambo hilo, wala halikunijia akilini mwangu. Kwa sababu hiyo, siku zaja ambapo hawataliita tena ‘Tofethi,’ au ‘Bonde la Mwana wa Hinomu,’ bali wataliita ‘Bonde la Mauaji.’ Huko ndiko watakakozika watu, kwa sababu hapatakuwa na mahali pengine pa kuzikia. Maiti za watu hao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa porini, na hapatakuwa na mtu atakayewafukuza. Nchi itakuwa jangwa na katika miji ya Yuda na mitaa ya Yerusalemu nitakomesha sauti zote za vicheko na furaha, sauti za bwana arusi na bibi arusi, kwa sababu nchi itakuwa ukiwa. “Wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, mifupa ya wafalme wa Yuda, mifupa ya wakuu wao, mifupa ya makuhani, mifupa ya manabii na mifupa ya wakazi wote wa Yerusalemu itachimbuliwa makaburini mwao. Itaachwa imetandazwa mbele ya jua na mwezi na sayari zote za mbinguni, vitu ambavyo walivipenda na kuvitumikia, wakavitaka shauri na kuviabudu. Mifupa hiyo haitakusanywa wala kuzikwa, bali itakuwa kama mavi juu ya ardhi. Watu wote waliobaki wa jamaa hii mbovu, mahali popote pale nilipowatawanya, wataona heri kufa kuliko kuishi. Ndivyo nisemavyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi. “Wewe Yeremia utawaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mtu akianguka, je hainuki tena? Mtu akipotea, je, hairudii tena njia yake? Mbona basi, watu hawa wameacha njia iliyo sawa na kuendelea katika upotovu wao? Wanashikilia miungu yao ya uongo, na kukataa kunirudia mimi! Mimi nilisikiliza kwa makini, lakini wao hawakusema ukweli wowote. Hakuna mtu anayetubu uovu wake, wala kujiuliza; ‘Nimefanya nini?’ Kila mmoja wao anashika njia yake, kama farasi akimbiliavyo moja kwa moja vitani. Hata korongo anajua wakati wa kuhama; njiwa, mbayuwayu na koikoi, hufuata majira yao ya kurudi. Lakini watu wangu hawa hawajui kitu juu ya amri zangu mimi Mwenyezi-Mungu. Mnawezaje kusema: ‘Sisi tuna hekima, sisi tunayo sheria ya Mwenyezi-Mungu,’ hali waandishi wa sheria, wameipotosha sheria yangu? Wenye hekima wenu wataaibishwa; watafadhaishwa na kunaswa. Wamelikataa neno la Mwenyezi-Mungu; je, ni hekima gani hiyo waliyo nayo? Kwa hiyo, wake zao nitawapa watu wengine, mashamba yao nitawapa wengine. Maana, tangu mdogo hadi mkubwa, kila mmoja ana tamaa ya faida haramu. Tangu manabii hadi makuhani, kila mmoja anatenda kwa udanganyifu. Wameliponya jeraha la watu wangu juujuu, wakisema, ‘Kuna amani, kuna amani’, kumbe hakuna amani yoyote! Je, waliona aibu walipotenda machukizo hayo? La hasha! Hawakuona aibu hata kidogo. Hata hawajui kuona haya. Kwa hiyo, wataanguka pamoja na wale walioanguka; nitakapowaadhibu, wataangamia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema: Nilipotaka kukusanya chochote kutoka kwao, sikupata zabibu hata moja juu ya mzabibu, sikupata tini zozote juu ya mtini; hata majani yao yamekauka. Hata nilichokuwa nimewapa kimetoweka.” “Watu wanauliza: Kwa nini sisi tunakaa tu hapa? Kusanyikeni, tuingie katika miji yenye ngome, tukaangamie huko! Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametupangia tuangamie, ametupa maji yenye sumu tunywe, kwa kuwa tumemkosea yeye. Tulitazamia kupata amani, lakini hakuna jema lililotokea. Tulitazamia wakati wa kuponywa, badala yake tukapata vitisho. Sauti za farasi wao zinasikika, kwa mlio wa farasi wao wa vita, nchi nzima inatetemeka. Wanafika na kuiharibu nchi na vyote vilivyomo, kuangamiza mji pamoja na wote waishio humo. “Basi nitawaleteeni nyoka; nyoka wenye sumu wasioweza kurogwa na walozi, nao watawauma nyinyi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Huzuni yangu haiwezi kutulizwa, moyo wangu wasononeka ndani yangu. Sikiliza kilio cha watu wangu, kutoka kila upande katika nchi. “Je, Mwenyezi-Mungu hayuko Siyoni? Je, mfalme wake hayuko tena huko?” “Mbona wamenikasirisha kwa sanamu zao za miungu, na vinyago vyao vya miungu ya kigeni?” “Mavuno yamepita, kiangazi kimekwisha, nasi bado hatujaokolewa! Jeraha la watu wangu limeniumiza moyoni, ninaomboleza na kufadhaika. Je, hakuna dawa ya kupaka huko Gileadi? Je, hakuna mganga huko? Mbona basi watu wangu hawajaponywa? Laiti kichwa changu kingekuwa kisima cha maji, na macho yangekuwa chemchemi ya machozi ili nipate kulia mchana na usiku, kwa ajili ya watu wangu waliouawa! Laiti ningekuwa na mahali pa kukaa jangwani, ambamo ningewaacha watu wangu na kwenda zangu.” Mwenyezi-Mungu asema: “Wote ni watu wazinzi, ni genge la watu wahaini. Hupinda maneno yao kama pinde; wameimarika kwa uongo na si kwa haki. Huendelea kutoka uovu hata uovu, wala hawanitambui mimi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Kila mmoja ajihadhari na jirani yake! Hata ndugu yeyote haaminiki, kila ndugu ni mdanganyifu, na kila jirani ni msengenyaji. Kila mmoja humdanganya jirani yake, hakuna hata mmoja asemaye ukweli. Wamezifundisha ndimi zao kusema uongo; hutenda uovu kiasi cha kushindwa kabisa kutubu. Wanarundika dhuluma juu ya dhuluma, na udanganyifu juu ya udanganyifu. Wanakataa kunitambua mimi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Tazama, nitawayeyusha na kuwajaribu! Au, nifanye nini zaidi na watu wangu waovu? Ndimi zao ni kama mishale yenye sumu, daima haziishi kudanganya; kila mmoja huongea vema na jirani yake, lakini moyoni mwake hupanga kumshambulia. Je, nisiwaadhibu kwa sababu ya mambo haya? Je, nisilipe kisasi kwa taifa kama hili? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Nitaililia na kuiomboleza milima; nitayaombolezea malisho nyikani, kwa sababu yamekauka kabisa, hakuna mtu apitaye mahali hapo. Hakusikiki tena sauti za ng'ombe; ndege na wanyama wamekimbia na kutoweka. Mwenyezi-Mungu asema: “Nitaifanya Yerusalemu magofu matupu, naam, nitaifanya kuwa pango la mbweha; na miji ya Yuda nitaifanya kuwa jangwa, mahali pasipokaliwa na mtu yeyote.” Nami nikauliza, “Je kuna mtu mwenye hekima kiasi cha kuweza kueleza mambo haya? Mwenyezi-Mungu aliongea na nani hata huyo aweze kutangaza kitu hicho? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa tupu kama jangwa hata hakuna mtu apitaye humo?” Mwenyezi-Mungu akajibu: “Kwa kuwa wamekataa kushika sheria yangu niliyowapa, wamekataa kutii sauti yangu na kufuata matakwa yake. Badala yake wamefuata kwa ukaidi fikira za mioyo yao, wakaenda kuyaabudu Mabaali kama walivyofundishwa na wazee wao. Basi, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Tazama nitawalisha watu hawa uchungu na kuwapa maji yenye sumu wanywe. Nitawatawanya kati ya mataifa ambayo wao wenyewe wala wazee wao hawakupata kuyajua; nitawafanya waandamwe na vita mpaka hapo nitakapowaangamiza wote.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Fikirini na kuwaita wanawake waomboleze; naam, waiteni wanawake hodari wa kuomboleza. Waambieni: ‘Njoni hima mkaomboleze juu yetu, macho yetu yapate kuchuruzika machozi, na kope zetu zibubujike machozi kama maji.’” Kilio kinasikika Siyoni: “Tumeangamia kabisa! Tumeaibishwa kabisa! Lazima tuiache nchi yetu, maana nyumba zetu zimebomolewa! Enyi wanawake, sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu! Tegeni masikio msikie jambo analosema. Wafundisheni binti zenu kuomboleza, na jirani zenu wimbo wa maziko: ‘Kifo kimepenya madirisha yetu, kimeingia ndani ya majumba yetu; kimewakatilia mbali watoto wetu barabarani, vijana wetu katika viwanja vya mji. Maiti za watu zimetapakaa kila mahali kama marundo ya mavi mashambani, kama masuke yaliyoachwa na mvunaji, wala hakuna atakayeyakusanya.’ Ndivyo alivyoniambia Mwenyezi-Mungu niseme.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mwenye hekima asijivunie nguvu zake, wala tajiri asijivunie utajiri wake. Anayetaka kujivuna na ajivunie jambo hili: Kwamba ananifahamu kwamba anajua Mwenyezi-Mungu hutenda mema, hufanya mambo ya haki na uadilifu duniani. Watu wa namna hiyo ndio wanipendezao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo nitawaadhibu wote waliotahiriwa mwilini tu: Wamisri, Wayuda, Waedomu, Waamoni, Wamoabu na wakazi wote wa jangwani wanaonyoa denge. Maana watu hawa wote na Waisraeli wote hawakutahiriwa moyoni.” Sikilizeni neno analowaambieni Mwenyezi-Mungu, enyi Waisraeli! Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Msijifunze mienendo ya mataifa mengine, wala msishangazwe na ishara za mbinguni; yaacheni mataifa mengine yashangazwe nazo. Maana, mila za dini za watu hawa ni za uongo. Mtu hukata mti msituni fundi akachonga kinyago cha mungu kwa shoka. Kisha watu hukipamba kwa fedha na dhahabu wakakipigilia misumari kwa nyundo ili kisije kikaanguka. Vinyago vyao ni kama vinyago vya kutishia ndege katika shamba la matango, havina uwezo wa kuongea; ni lazima vibebwe maana haviwezi kutembea. Msiviogope vinyago hivyo, maana haviwezi kudhuru, wala haviwezi kutenda lolote jema.” Ee Mwenyezi-Mungu, hakuna aliye kama wewe; wewe ni mkuu na nguvu yako yajulikana. Nani asiyekuogopa wewe, ee mfalme wa mataifa? Wewe wastahili kuheshimiwa. Miongoni mwa wenye hekima wote wa mataifa, na katika falme zao zote, hakuna hata mmoja aliye kama wewe. Wote ni wajinga na wapumbavu mafunzo ya vinyago ni upuuzi mtupu! Vinyago hivyo hupambwa kwa fedha kutoka Tarshishi, na dhahabu kutoka Ofiri; kazi ya mafundi stadi na wafua dhahabu. Zimevishwa nguo za samawati na zambarau, zilizofumwa na wafumaji stadi. Lakini Mwenyezi-Mungu ni Mungu wa kweli; Mungu aliye hai, mfalme wa milele. Akikasirika, dunia hutetemeka, mataifa hayawezi kustahimili hasira yake. Basi, utawaambia hivi: “Miungu ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia. Itatoweka kabisa duniani na chini ya mbingu.” Mwenyezi-Mungu aliiumba dunia kwa nguvu zake; kwa hekima yake aliuimarisha ulimwengu, kwa akili yake alizitandaza mbingu. Anapotoa sauti yake, maji hunguruma mbinguni, huzusha ukungu kutoka mipaka ya dunia. Huufanya umeme umulike wakati wa mvua, na kuutoa upepo katika ghala zake. Binadamu ni mjinga na mpumbavu; kila mfua dhahabu huaibishwa na vinyago vyake; maana, vinyago hivyo ni uongo mtupu. Havina uhai wowote ndani yao. Havina thamani, ni udanganyifu mtupu; wakati vitakapoadhibiwa vyote vitaangamia. Lakini Mungu wa Yakobo si kama vinyago hivyo, maana, yeye ndiye aliyeumba vitu vyote, na Israeli ni taifa lililo mali yake; Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndilo jina lake. Kusanyeni vitu vyenu enyi watu mliozingirwa. Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wakati huo nitawatupa nje ya nchi hii, nitawataabisha asibaki mtu yeyote.” Ole wangu mimi Yerusalemu maana nimejeruhiwa! Jeraha langu ni baya sana! Lakini nilisema: “Hakika haya ni mateso, na sina budi kuyavumilia.” Lakini hema langu limebomolewa, kamba zake zote zimekatika; watoto wangu wameniacha, na kwenda zao, wala hawapo tena; hakuna wa kunisimikia tena hema langu, wala wa kunitundikia mapazia yangu. Nami Yeremia nikasema: Wachungaji wamekuwa wajinga, hawakuomba shauri kwa Mwenyezi-Mungu; kwa sababu hiyo, hawakufanikiwa, na kondoo wao wote wametawanyika. Sikilizeni sauti! Habari zinatufikia. Kuna kishindo kutoka kaskazini. Taifa kutoka kaskazini linakuja, kuifanya miji ya Yuda kuwa jangwa ambamo kutakuwa na mapango ya mbweha! Najua, ee Mwenyezi-Mungu, binadamu hana uwezo na maisha yake; hakuna mtu awezaye kuyaongoza maisha yake. Utukosoe, ee Mwenyezi-Mungu, lakini si kwa ghadhabu, wala kwa hasira yako, tusije tukaangamia. Imwage hasira yako juu ya mataifa yasiyokuabudu, na juu ya watu ambao hawakutambui. Maana, wamewaua wazawa wa Yakobo; wamewaua na kuwaangamiza kabisa, na nchi yao wameiacha magofu. Neno lilimjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu; “Sikiliza masharti ya agano hili, kisha nenda ukawatangazie watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu. Utawaambia hivi: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: Na alaaniwe mtu yeyote asiyejali masharti ya agano hili. Hili ni agano nililowapa wazee wenu nilipowatoa nchini Misri, kutoka katika tanuri la chuma. Niliwaambia wanitii na kufanya yote niliyowaamuru, na kwamba wakifanya hivyo, watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Wakifuata masharti hayo, mimi nitatimiza ahadi niliyowapa wazee wenu, kwamba nitawapa nchi inayotiririka maziwa na asali, kama ilivyo hadi leo.” Nami nikajibu: “Na iwe hivyo, ee Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Tangaza masharti hayo yote katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Waambie watu wayasikilize masharti ya agano hili na wayatekeleze. Maana niliwaonya vikali wazee wao nilipowatoa katika nchi ya Misri, na nimeendelea kuwaonya wanitii mpaka siku hii ya leo. Lakini wao hawakunitii, wala hawakunisikiliza. Badala yake, kila mmoja wao alizidi kuwa mkaidi na mwovu. Basi, niliwaadhibu kulingana na masharti ya agano hili nililowaamuru walishike, lakini hao wakakataa kulishika.” Tena Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu wanafanya njama za kuniasi. Wameurudia uovu wa wazee wao ambao walikataa kusikiliza maneno yangu; wameiabudu miungu mingine na kuitumikia. Watu wa Israeli na watu wa Yuda wamevunja agano nililofanya na wazee wao. Kwa hiyo, sasa, mimi Mwenyezi-Mungu ninawaonya kwamba nitawaletea maafa ambayo hawataweza kuepukana nayo. Hata kama wakinililia namna gani, sitawasikiliza. Hapo ndipo watu wa Israeli na Yerusalemu watakapoiendea miungu yao ambayo wanaifukizia ubani. Lakini miungu hiyo haitaweza kuwaokoa wakati huo wa taabu zao. Miungu yako, ewe Yuda imekuwa mingi kama ilivyo miji yako; kama zilivyo nyingi barabara za Yerusalemu, ndivyo zilivyo nyingi madhabahu walizomjengea mungu kinyaa Baali, ili kumfukizia ubani. Basi, wewe Yeremia, usiwaombee watu hawa, usinililie kwa ajili yao, wala usiwaombee dua. Maana, hata wakiniomba wanapotaabika, mimi sitawasikiliza.” Mwenyezi-Mungu asema: “Watu niwapendao wana haki gani kuingia hekaluni mwangu wakati wametenda maovu? Je, wanadhani nadhiri na nyama zilizowekwa wakfu zitawaondolea maafa? Je, hayo yatawafurahisha? Wakati fulani, mimi nilisema, wao ni mzeituni wenye majani mabichi, mzeituni mzuri na wenye matunda mema; lakini sasa, kwa ngurumo ya dhoruba kubwa, nitauchoma moto na kuyateketeza matawi yake. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi niliuotesha huu mzeituni; lakini natangaza maafa dhidi yake kwa sababu ya maovu ambayo watu wa Israeli na Yuda wameyafanya. Wamenikasirisha kwa kumfukizia ubani mungu Baali.” Mwenyezi-Mungu alinijulisha, nami nikaelewa; Mwenyezi-Mungu alinijulisha njama zao. Nami nilikuwa kama kondoo mpole anayepelekwa machinjoni; sikujua kuwa njama walizofanya zilikuwa dhidi yangu. Walisema: “Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, tumkatilie mbali kutoka nchi ya walio hai, kamwe jina lake lisikumbukwe tena.” Lakini, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, wewe unayehukumu kwa haki, unayepima mioyo na akili za watu, unijalie kuona ukiwalipiza kisasi, maana kwako nimekiweka kisa changu. Ndiyo maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi anacho cha kusema juu ya watu wa Anathothi ambao wanataka kuniua na kuniambia: “Usitoe unabii kwa jina la Mwenyezi-Mungu, la sivyo tutakuua.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Nitawaadhibu watu hao. Vijana wao watauawa vitani; watoto wao wa kiume na wa kike watakufa kwa njaa. Nimepanga muda wa kuleta maangamizi juu ya watu wa Anathothi. Wakati huo utakapofika, hakuna hata mmoja wao atakayebaki hai.” Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ni mwadilifu, ingawa nakulalamikia. Lakini ningependa kutoa hoja zangu mbele yako: Kwa nini waovu hufanikiwa katika mambo yao? Mbona wote wenye hila hustawi? Unawaotesha nao wanaota; wanakua na kuzaa matunda. Wanakutaja kwa maneno yao, lakini mioyo yao iko mbali nawe. Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu wanijua; wayathibiti maelekeo yangu kwako. Uwaokote hao kama kondoo wa kuchinjwa, watenge kwa ajili ya wakati wa kuuawa. Mpaka lini nchi itaomboleza kwa ukame, na nyasi za mashamba yote kunyauka? Wanyama na ndege wanakufa kwa uovu wa wakazi wake; wanasema: “Mungu hataona mwisho wetu.” Mwenyezi-Mungu asema, “Ikiwa umeshindana na waendao kwa miguu ukachoka, utawezaje kushindana na farasi? Kama unaanguka katika nchi isiyo na vizuizi, utafanyaje katika msitu wa Yordani? Hata ndugu zako, jamaa yako mwenyewe, nao pia wamekutendea mambo ya hila; wanakukemea waziwazi. Usiwaamini hata kidogo, japo wanakuambia maneno mazuri.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nimeiacha nyumba yangu; nimeitupa mali yangu mimi mwenyewe. Israeli, mpenzi wangu wa moyo, nimemtia mikononi mwa maadui zake. Wateule wangu wamenigeuka, wamekuwa kama simba porini, wameningurumia mimi; ndiyo maana nawachukia. Wateule wangu wamekuwa ndege mzuri wanaoshambuliwa na kozi pande zote. Nenda ukawakusanye wanyama wote wakali waje kushiriki katika karamu. Wachungaji wengi wameharibu shamba langu la mizabibu, wamelikanyagakanyaga chini lililo mali yangu; shamba langu zuri wamelifanya jangwa. Wamelifanya kuwa tupu; katika ukiwa wake lanililia. Nchi yote imekuwa jangwa, wala hakuna mtu anayejali. Juu ya milima yote jangwani, watu wamefika kuangamiza. Upanga wangu unapita kuiangamiza nchi, toka upande mmoja hadi mwingine, wala hakuna mtu atakayeishi kwa amani. Walipanda ngano, lakini walivuna magugu; walifanya bidii, lakini hawakupata kitu. Kwa sababu ya hasira yangu kali, mavuno watakayoyapata yatakuwa aibu tupu.” Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya jirani wabaya wa watu wangu: “Wamekigusa kile kilicho changu, kile nilichowapa watu wangu Israeli! Basi nitawangoa kutoka katika nchi yao. Hata watu wa Yuda nitawangoa katika nchi yao. Lakini baada ya kuwangoa, nitawahurumia tena; nitalirudisha kila taifa katika sehemu yake na katika nchi yake. Na kama watajifunza njia za watu wangu kwa moyo wote, kama wataapa kwa jina langu kwa kusema, ‘Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu,’ kama vile walivyowafundisha watu wangu kuapa kwa jina la mungu Baali, basi watajengeka miongoni mwa watu wangu. Lakini taifa lolote ambalo halitanitii, nitalingoa kabisa na kuliangamiza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Nenda ukajinunulie kikoi cha kitani, ukajifunge kiunoni; lakini usikitie majini.” Basi, nikaenda, nikanunua kikoi kama alivyoniagiza Mwenyezi-Mungu, nikajifunga kiunoni. Kisha, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili: “Kichukue kikoi ulichonunua na ambacho umejifunga kiunoni, uende kwenye mto Eufrate na kukificha katika pango mwambani.” Basi, nikaenda na kukificha kikoi hicho karibu na mto Eufrate, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniamuru. Ikawa, baada ya siku nyingi, Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Nenda kwenye mto Eufrate, ukakichukue kile kikoi nilichokuamuru ukifiche huko.” Basi, nikaenda kwenye mto Eufrate, nikachimbua na kukitoa kile kikoi mahali nilipokuwa nimekificha. Nilipokitoa, nilishangaa kukiona kuwa kilikuwa kimeharibika kabisa; kilikuwa hakifai tena. Ndipo neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hivi ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikubwa cha Yerusalemu. Watu hawa waovu wanakataa kusikia maneno yangu, na badala yake wanakuwa wakaidi na kufuata mawazo yao wenyewe. Wanaifuata miungu mingine, wanaitumikia na kuiabudu. Hao watakuwa kama kikoi hiki ambacho hakifai kitu. Kama vile kikoi kinavyoshikamana na kiuno cha mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami watu wa Israeli na watu wa Yuda, ili wajulikane kwa jina langu, wanisifu na kunitukuza. Lakini wao hawakunisikiliza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliniambia hivi: “Waambie watu wa Israeli kwamba kila mtungi utajazwa divai. Lakini utakapowaambia hivyo, wao watakujibu hivi: ‘Kwani unadhani sisi hatujui kwamba kila mtungi utajazwa divai?’ Nawe utawaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawalewesha wenyeji wote wa nchi hii; wafalme wanaotawala mahali pa Daudi, makuhani, manabii na wakazi wote wa Yerusalemu. Nitawagonganisha wao kwa wao kina baba na watoto. Sitawahurumia, sitawaachia wala sitawarehemu, bali nitawaangamiza.” Enyi Waisraeli, sikilizeni kwa makini, msiwe na majivuno maana Mwenyezi-Mungu anasema nanyi. Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kabla hajawaletea giza, nanyi mkajikwaa miguu kwenye milima ya giza. Nyinyi mnatazamia mwanga, lakini anaugeuza kuwa utusitusi na kuufanya kuwa giza nene. Lakini kama msiponisikiliza, moyo wangu utalia machozi faraghani, kwa sababu ya kiburi chenu. Nitalia kwa uchungu na kububujika machozi, kwa kuwa watu wa Mwenyezi-Mungu wametekwa. Mwambie mfalme na mama yake hivi: “Shukeni kwenye viti vyenu vya enzi, maana taji zenu nzuri zimeanguka vichwani mwenu. Miji ya Negebu imezingirwa; hakuna awezaye kufungua malango yake. Watu wa Yuda wamechukuliwa mateka, wote kabisa wamepelekwa utumwani.” Inua macho yako, ee Yerusalemu! Tazama! Madui zako waja kutoka kaskazini. Kundi ulilokabidhiwa liko wapi? Kundi lako zuri li wapi? Utasemaje juu ya wale uliodhani ni rafiki, wale ambao wewe mwenyewe uliwafundisha, watakapokushinda na kukutawala? Je, si utakumbwa na uchungu kama wa mama anayejifungua? Nawe utajiuliza moyoni mwako, “Kwa nini mambo haya yamenipata?” Sawa! Kama vazi lako limepandishwa juu, nawe ukatendewa kwa ukatili mno, hayo ni matokeo ya makosa yako mengi mno. Je, Mwethiopia aweza kubadili rangi yake, au chui madoadoa yake? Ikiwezekana, nanyi pia mnaweza kutenda mema, nyinyi mliozoea kutenda maovu! Mwenyezi-Mungu atawatawanya kama makapi yanayopeperushwa na upepo kutoka jangwani. Mwenyezi-Mungu asema: “Hayo ndiyo yatakayokupata, ndivyo nilivyoamua kukutenda mimi Mwenyezi-Mungu, kwa sababu umenisahau mimi, ukaamini miungu ya uongo. Nitalipandisha vazi lako hadi kichwani na aibu yako yote itaonekana wazi. Nimeyaona machukizo yako: Naam, uzinifu wako na uzembe wako, na uasherati wako wa kupindukia, juu ya milima na mashambani. Ole wako ee Yerusalemu! Mpaka lini utakaa bila kutakaswa?” Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia kuhusu ule ukame: “Watu wa Yuda wanaomboleza, na malango yao yanalegea. Watu wake wanaomboleza udongoni na kilio cha Yerusalemu kinapanda juu. Wakuu wake wanawatuma watumishi wao maji; watumishi wanakwenda visimani, lakini maji hawapati; wanarudi na vyombo vitupu. Kwa aibu na fadhaa wanafunika vichwa vyao. Wakulima wanahuzunika na kufunika vichwa vyao kwa kuona jinsi ardhi ilivyonyauka. Hata kulungu porini anamwacha mtoto wake mchanga, kwa sababu hakuna nyasi. Pundamwitu wanasimama juu ya vilele vikavu, wanatweta kwa kukosa hewa kama mbweha; macho yao yanafifia kwa kukosa chakula. “Nao watu wanasema: Ingawa dhambi zetu zashuhudia dhidi yetu, utusaidie ee Mwenyezi-Mungu kwa heshima ya jina lako. Maasi yetu ni mengi, tumetenda dhambi dhidi yako. Ewe uliye tumaini la Israeli, mwokozi wetu wakati wa taabu, utakuwaje kama mgeni nchini mwetu, kama msafiri alalaye usiku mmoja? Utakuwaje kama mtu uliyechanganyikiwa, kama shujaa asiyeweza kusaidia mtu? Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu, u pamoja nasi; sisi twaitwa kwa jina lako, usituache.” Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya watu hawa: “Kweli wamependa sana kutangatanga, wala hawakujizuia; kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu siwapokei. Sasa nitayakumbuka makosa yao, na kuwaadhibu kwa dhambi zao.” Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Usiwaombee watu hawa fanaka. Hata wakifunga, sitayasikiliza maombi yao, na hata wakinitolea sadaka za kuteketeza na za nafaka, mimi sitazikubali. Bali nitawaangamiza kwa upanga, njaa na tauni.” Kisha mimi nikasema, “Tazama, ee Bwana Mwenyezi-Mungu! Manabii wanawaambia watu hawa kwamba hapatakuwa na vita wala njaa, kwa sababu umeahidi kuwa patakuwa na amani tu katika nchi yetu.” Naye Mwenyezi-Mungu, akaniambia: “Hao manabii wanatoa unabii wa uongo kwa jina langu. Mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi yasiyo na maana yoyote, uongo wanaojitungia wenyewe. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi kuhusu hao manabii wanaotabiri kwa jina langu, ingawa mimi sikuwatuma, na wanaosema kwamba hapatakuwa na vita wala njaa katika nchi hii: Manabii hao wataangamia kwa upanga na kwa njaa. Na hao ambao waliwatabiria mambo hayo, watatupwa nje katika barabara za Yerusalemu wakiwa wamekufa kwa njaa na vita, wala hapatakuwa na mtu wa kuwazika. Hayo yatawapata wao wenyewe, wake zao, watoto wao wa kike na wa kiume; maana mimi nitawamwagia uovu wao wenyewe. Hivi ndivyo utakavyowaambia: Laiti macho yangetoa machozi kutwa kucha, wala yasikome kububujika, maana, watu wangu wamejeruhiwa vibaya, wamepata pigo kubwa sana. Nikienda nje mashambani, naiona miili ya waliouawa vitani; nikiingia ndani ya mji, naona tu waliokufa kwa njaa! Manabii na makuhani wanashughulikia mambo yao nchini, wala hawajui wanalofanya.” Ee Mwenyezi-Mungu, je, umemkataa Yuda kabisa? Je, moyo wako umechukizwa na Siyoni? Kwa nini umetupiga vibaya, hata hatuwezi kupona tena? Tulitazamia amani, lakini hatukupata jema lolote; tulitazamia wakati wa kuponywa, badala yake tukapata vitisho. Tunakiri uovu wetu, ee Mwenyezi-Mungu, tunakiri uovu wa wazee wetu, maana, tumekukosea wewe. Usitutupe, kwa heshima ya jina lako; usikidharau kiti chako cha enzi kitukufu. Ukumbuke agano ulilofanya nasi, wala usilivunje. Je miungu ya uongo ya mataifa yaweza kuleta mvua? Au, je, mbingu zaweza kutoa manyunyu? Je, si wewe ee Mwenyezi-Mungu uliye Mungu wetu? Tunakuwekea wewe tumaini letu, maana wewe unayafanya haya yote. Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Hata kama Mose na Samueli wangesimama mbele yangu na kunisihi, nisingewahurumia watu hawa. Waondoe kabisa mbele yangu. Waache waende zao! Na wakikuuliza, ‘Twende wapi?’ wewe utawajibu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Waliopangiwa kufa kwa maradhi, watakufa kwa maradhi; waliopangiwa kufa kwa upanga, watakufa kwa upanga; waliopangiwa kufa kwa njaa, watakufa kwa njaa; na waliopangiwa kuwa mateka, watatekwa mateka. Mimi Mwenyezi-Mungu nimeamua kuwaletea aina nne za maangamizi: Vita itakayowaua, mbwa watakaowararua; ndege wa angani watakaowadonoa na wanyama wa porini watakaowatafuna na kuwamaliza. Nitawafanya kuwa kitu cha kutisha kwa falme zote za dunia, kwa sababu ya mambo ambayo Manase mwana wa Hezekia, aliyafanya huko Yerusalemu, alipokuwa mfalme wa Yuda. “Ni nani atakayewahurumia, enyi watu wa Yerusalemu? Ni nani atakayeomboleza juu yenu? Nani atasimama kuuliza habari zenu? Nyinyi mmenikataa mimi, nasema mimi Mwenyezi-Mungu; nyinyi mmeniacha mkarudi nyuma. Hivyo nimenyosha mkono kuwaangamiza, kwa kuwa nimechoka kuwahurumia. Nimewapepeta kwa chombo cha kupuria, katika kila mji nchini; nimewaangamiza watu wangu, kwa kuwaulia mbali watoto wao, lakini hawakuacha njia zao. Wajane wao wamekuwa wengi kuliko mchanga wa bahari. Kina mama wa watoto walio vijana nimewaletea mwangamizi mchana. Nimesababisha uchungu na vitisho viwapate kwa ghafla. Mama aliyesifika kuwa na watoto saba; sasa ghafla hana kitu. Ametoa pumzi yake ya mwisho, jua lake limetua kukiwa bado mchana; ameaibishwa na kufedheheshwa. Na wale waliobaki hai nitawaacha wauawe kwa upanga na maadui zao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa! Mimi nimekuwa mtu wa ubishi na ugomvi nchini pote! Sijapata kukopesha mtu wala kukopeshwa na mtu, lakini kila mtu ananiapiza. Haya basi, ee Mwenyezi-Mungu, acha laana hizo nizipate kama sijakutumikia vema na kama sikukusihi kwa ajili ya maadui zangu wakati walipokuwa katika taabu na shida! Je, mtu aweza kuvunja chuma, chuma kitokacho kaskazini, au shaba? Mwenyezi-Mungu asema: “Nitaifanya mali yenu na hazina zenu zichukuliwe nyara tena bila kulipwa fidia yoyote kwa sababu ya dhambi zenu zote mlizotenda kila mahali nchini. Nitawafanya muwatumikie maadui zenu katika nchi msiyoijua kwa sababu hasira yangu imewaka moto ambao hautazimwa milele.” Nami nikasema: “Lakini wewe Mwenyezi-Mungu wajua; unikumbuke na kuja kunisaidia. Nilipizie kisasi watesi wangu. Wewe u mvumilivu, usiniache niangamie; kumbuka kuwa ninatukanwa kwa ajili yako. Mara maneno yako yalipofika, niliyameza; nayo yakanifanya niwe na furaha, yakawa utamu moyoni mwangu, maana mimi najulikana kwa jina lako, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Sikuketi pamoja na wanaostarehe, wala sikufurahi pamoja nao. Niliketi peke yangu nimelemewa nguvu yako; kwa maana ulinijaza hasira yako. Kwa nini mateso yangu hayaishi? Mbona jeraha langu haliponi, wala halitaki kutibiwa? Ama kweli umenidanganya, kama kijito cha maji ya kukaukakauka!” Mwenyezi-Mungu akajibu: “Kama ukinirudia nitakurudishia hali ya kwanza, nawe utanitumikia tena. Kama ukisema maneno ya maana na sio ya upuuzi, basi utakuwa msemaji wangu. Watu watakuja kujumuika nawe, wala sio wewe utakayekwenda kwao. Mbele ya watu hawa, nitakufanya ukuta imara wa shaba. Watapigana nawe, lakini hawataweza kukushinda, maana, mimi niko pamoja nawe, kukuokoa na kukukomboa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitakuokoa mikononi mwa watu waovu, na kukukomboa makuchani mwa wakatili.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia na kusema: “Wewe hutaoa wala hutapata watoto mahali hapa. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu ya watoto wa kiume na wa kike watakaozaliwa mahali hapa, na juu ya wazazi wao: Hao watakufa kwa maradhi mabaya, na hakuna atakayewaombolezea wala kuwazika. Maiti zao zitazagaa kama mavi juu ya ardhi. Wataangamia kwa upanga na kwa njaa; na maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wakali wa nchi. “Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Usiingie kabisa katika nyumba ya matanga wala usiende kuomboleza wala kuwalilia. Kwa maana nimeondoa amani yangu, fadhili zangu na huruma yangu kutoka kwa watu hawa. Wote, wakubwa kwa wadogo, watakufa katika nchi hii; nao hawatazikwa, wala hakuna atakayewaombolezea. Hakuna atakayejikatakata au kunyoa upara wa matanga. Hakuna atakayemshirikisha aliyefiwa chakula cha kumfariji, wala kumpatia kinywaji cha kumfariji anywe kwa ajili ya kufiwa na mama au baba yake. “Usiingie katika nyumba wanamofanya karamu. Usiketi kula na kunywa pamoja nao. Maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nitazikomesha kabisa kutoka mahali hapa sauti za furaha na za shangwe, pamoja na sauti za bwana arusi na bibi arusi. Yote haya nitayafanya wakati wa uhai wenu mkiwa mnaona waziwazi. Nawe utakapowaambia watu hao maneno haya yote, wao watakuuliza, ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ametamka uovu huu mkubwa dhidi yetu? Tumefanya kosa gani? Tumetenda dhambi gani dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu?’ Nawe utawajibu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wazee wenu waliniacha, wakaifuata miungu mingine, wakaitumikia na kuiabudu. Waliniacha, wala hawakuzitii sheria zangu. Nyinyi mmefanya vibaya zaidi kuliko wazee wenu, maana kila mmoja wenu ni mkaidi na mwenye nia mbaya, wala hamnisikilizi. Kwa hiyo, nitawatupilia mbali kutoka nchi hii mpaka kwenye nchi ambayo nyinyi wenyewe wala wazee wenu hawakuijua. Huko mtaitumikia miungu mingine usiku na mchana, wala sitawafadhili. “Kwa hiyo siku zaja, nasema mimi Mwenyezi-Mungu ambapo watu hawataapa tena kwa kusema, ‘Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu aliyewatoa watu wa Israeli kutoka nchini Misri’; bali wataapa kwa kusema, ‘Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu aliyewatoa Waisraeli kutoka nchi ya kaskazini na kutoka katika nchi zote alikowafukuzia!’ Maana, nitawarudisha katika nchi yao niliyowapa wazee wao.” Mwenyezi-Mungu asema: “Tazama, nitaita wavuvi wengi waje kuwakamata watu hawa. Kisha, nitaita wawindaji wengi watakaowawinda katika kila mlima, kila kilima na katika mapango ya miambani. Maana, mimi nayaona matendo yao yote. Hakuna chochote kilichofichika kwangu. Makosa yao yote ni wazi mbele yangu. Nitalipiza kisasi maradufu juu ya dhambi zao na makosa yao kwa sababu wameitia unajisi nchi yangu kwa mizoga ya miungu yao ya kuchukiza, wakaijaza hii nchi yangu machukizo yao.” Ee Mwenyezi-Mungu! Wewe ndiwe nguvu yangu na ngome yangu; wewe ni kimbilio langu wakati wa taabu. Mataifa toka pande zote duniani yatakujia na kusema: “Wazee wetu hawakuwa na kitu ila miungu ya uongo, vitu duni visivyo na faida yoyote. Je, binadamu aweza kujitengenezea miungu? Basi, hao si miungu hata kidogo!” “Kwa hiyo,” asema Mwenyezi-Mungu, “wakati huu nitawafundisha watambue waziwazi nguvu zangu na uwezo wangu, nao watajua kwamba jina langu ni Mwenyezi-Mungu. “Dhambi ya watu wa Yuda, imeandikwa kwa kalamu ya chuma; kwa ncha ya almasi imechorwa mioyoni mwao na katika pembe za madhabahu zao, wakati watu wake wanakumbuka madhabahu zao na sanamu za mungu wa kike, Ashera, zilizowekwa kando ya miti mibichi juu ya vilele vya vilima, na juu ya milima katika sehemu tambarare. Mali yenu na hazina zenu zote nitazitoa zitekwe nyara kulipia dhambi zenu mlizotenda kila mahali nchini mwenu. Itawabidi muiachilie hiyo nchi yenu niliyowapeni, nami nitawafanya muwatumikie maadui zenu katika nchi msiyoijua, kwa sababu hasira yangu imewaka moto usiozimika milele.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Alaaniwe mtu anayemtegemea binadamu, mtu ambaye anategemea nguvu za binadamu, mtu ambaye moyo wake umeniacha mimi Mwenyezi-Mungu. Huyo ni kama kichaka jangwani, hataona chochote chema kikimjia. Ataishi mahali pakavu nyikani, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. “Abarikiwe mtu anayemtegemea Mwenyezi-Mungu, mtu ambaye Mwenyezi-Mungu ndiye tegemeo lake. Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya maji, upenyezao mizizi yake karibu na chemchemi. Hauogopi wakati wa joto ufikapo, majani yake hubaki mabichi. Hauhangaiki katika mwaka wa ukame, na hautaacha kuzaa matunda. “Moyo wa mtu ni mdanganyifu kuliko vitu vyote; hauwezi kuponywa, hakuna awezaye kuuelewa! Mimi Mwenyezi-Mungu hupima akili na kuchunguza mpaka ndani ya moyo wa mtu. Na hivyo humtendea kila mmoja, kulingana na mwenendo wake, kadiri ya matendo yake.” Mtu apataye mali isiyo halali ni kama kware akusanyaye makinda ambayo hakuyaangua: Wakati wa kilele cha ujana wake itamchopoka, na mwishoni atakuwa mtu mpumbavu. Kuna kiti cha enzi kitukufu kiti kilichoinuliwa juu; huko ndiko mahali petu patakatifu. Ee Mwenyezi-Mungu tumaini la Israeli, wote wanaokukataa wataaibishwa; wanaokuacha wewe watatoweka, kama majina yaliyoandikwa vumbini, kwa maana wamekuacha wewe Mwenyezi-Mungu, uliye chemchemi ya maji ya uhai. Uniponye, ee Mwenyezi-Mungu, nami nitapona; uniokoe, nami nitaokoka; maana, wewe ndiwe sifa yangu. Tazama watu wanavyoniambia: “Jambo alilotishia Mwenyezi-Mungu liko wapi? Acha basi lije!” Sikuikimbia huduma yako ya kuwa mchungaji wala sikutamani ile siku ya maafa ije. Wewe mwenyewe wajua nilichosema kwa mdomo wangu, nilichotamka wakijua waziwazi. Usiwe tisho kwangu; wewe ndiwe kimbilio langu siku ya maafa. Waaibishwe wale wanaonitesa, lakini mimi usiniache niaibike. Wafedheheshwe watu hao, lakini mimi usiniache nifedheheke. Uwaletee siku ya maafa, waangamize kwa maangamizi maradufu! Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Nenda ukasimame penye lango la watu ambapo wafalme wa Yuda huingia na kutoka mjini, na katika malango mengine yote ya Yerusalemu useme: Sikieni neno la Mwenyezi-Mungu enyi wafalme wa Yuda, nanyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu ambao huingia kwa kupitia malango haya. Waambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa usalama wa maisha yenu, muwe na hadhari msije mkabeba mzigo siku ya Sabato, au kuingiza mzigo mjini kupitia malango ya Yerusalemu. Msibebe mzigo kutoka majumbani mwenu siku ya Sabato wala kufanya kazi. Iadhimisheni siku ya Sabato kama siku takatifu kama nilivyowaamuru wazee wenu. Lakini wazee wenu hawakunisikiliza wala kujali, bali walivifanya vichwa vyao kuwa vigumu, wakakataa kusikia na kufuata maagizo yangu. “Lakini mkinisikiliza mimi Mwenyezi-Mungu, mkaacha kuingiza mzigo wowote kupitia malango ya mji huu siku ya Sabato, wala kufanya kazi siku hiyo, basi, wafalme na wana wa wafalme wanaomfuata mfalme Daudi katika utawala, pamoja na watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, wataingia kwa kupitia malango ya mji huu, wakiwa wamepanda farasi na magari ya farasi. Nao mji huu utakuwa na watu daima. Watu watakuja kutoka miji ya Yuda na maeneo ya kandokando ya Yerusalemu, kutoka nchi ya Benyamini, kutoka Shefela, kutoka nchi ya milima na kutoka Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa na tambiko, sadaka za nafaka na ubani wa harufu nzuri, pamoja na matoleo ya shukrani. Vyote hivyo watavileta katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Lakini msiponisikiliza na kuiadhimisha siku ya Sabato kama siku takatifu, msipoacha kubeba mizigo na kuingia nayo kupitia malango ya Yerusalemu siku ya Sabato, basi, nitawasha moto katika malango yake, nao utayateketeza majumba yote ya fahari ya Yerusalemu nao hautazimwa kamwe.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Yeremia, inuka uende nyumbani kwa mfinyanzi, na huko nitakupa maneno yangu.” Basi, nikateremka mpaka nyumbani kwa mfinyanzi, nikamkuta mfinyanzi akifanya kazi yake penye gurudumu la kufinyangia. Na ikawa kwamba chombo alichokifinyanga kilipoharibika mikononi mwake, yeye alifinyanga upya chombo kingine kadiri ilivyompendeza. Kisha, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Enyi Waisraeli! Je, mimi Mwenyezi-Mungu siwezi kuwafanya nyinyi kama alivyofanya mfinyanzi huyu? Jueni kuwa kama ulivyo udongo mikononi mwa mfinyanzi, ndivyo nyinyi mlivyo mikononi mwangu. Wakati wowote nitakapotoa tamko kuhusu taifa au ufalme kwamba nitalingoa na kulivunja na kuliangamiza, halafu taifa hilo likageuka na kuacha uovu wake, basi, mimi nitaacha kulitendea yale mambo niliyokusudia kulitendea. Hali kadhalika, wakati wowote nikitoa tamko kuhusu taifa au ufalme kwamba nitalijenga na kulistawisha, kisha taifa hilo likafanya uovu mbele yangu na kukataa kunitii, basi, mimi nitaacha kulitendea mema hayo niliyokusudia kulitendea. Sasa, basi, waambie watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi Hufinyanga jambo ovu dhidi yenu na kufanya mpango dhidi yenu. Rudini na kuacha njia zenu mbaya, mkarekebishe mienendo yenu na matendo yenu. Lakini wao watasema, ‘Hiyo ni bure tu! Tutafuata mipango yetu wenyewe na kila mmoja wetu atafanya kwa kiburi kadiri ya moyo wake mwovu.’” Basi, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Yaulize mataifa yote: Nani amewahi kusikia jambo kama hili. Israeli amefanya jambo la kuchukiza mno. Je, majabali ya Lebanoni hukosa theluji? Je, vijito vya maji vya milima yake hukauka? Lakini watu wangu wamenisahau mimi, wanafukizia ubani miungu ya uongo. Wamejikwaa katika njia zao, katika barabara za zamani. Wanapitia vichochoroni badala ya njia kuu. Wameifanya nchi yao kuwa kitisho, kitu cha kuzomewa daima. Kila mtu apitaye huko hushangaa na kutikisa kichwa chake. Nitawatawanya mbele ya adui, kama upepo utokao mashariki. Nitawapa kisogo badala ya kuwaonesha uso wangu siku hiyo ya kupata maafa yao.” Kisha, watu wakasema: “Njoni tumfanyie Yeremia njama, maana hatukosi makuhani wa kutufundisha, wenye hekima wa kutushauri na manabii wa kututangazia ujumbe wa Mungu! Njoni tumshtaki kwa maneno yake mwenyewe, wala tusiyatilie maanani yote asemayo.” Basi, mimi nikasali: Nitegee sikio ee Mwenyezi-Mungu, usikilize ombi langu. Je, mtu hulipwa mabaya kwa mema? Walakini, wamenichimbia shimo. Kumbuka nilivyosimama mbele yako, nikasema mema kwa ajili yao, ili kuiepusha hasira yako mbali nao. Kwa hiyo waache watoto wao wafe njaa, waache wafe vitani kwa upanga. Wake zao wawe tasa na wajane. Waume zao wafe kwa maradhi mabaya na vijana wao wachinjwe kwa upanga vitani. Kilio na kisikike majumbani mwao, unapowaletea kundi la wanyanganyi ghafla. Maana wamechimba shimo waninase; wameitegea mitego miguu yangu. Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wazijua njama zao zote za kuniua. Usiwasamehe uovu wao, wala kufuta dhambi zao. Waanguke chini mbele yako; uwakabili wakati wa hasira yako. Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Nenda ukanunue gudulia la udongo kwa mfinyanzi. Kisha, wachukue baadhi ya wazee wa watu na baadhi ya makuhani viongozi, halafu uende pamoja nao katika bonde la Mwana wa Hinomu, kwa kupitia lango la Vigae. Ukifika huko, tangaza maneno ninayokuambia. Utasema hivi: Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu enyi wafalme wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Kweli ninaleta maafa mabaya mahali hapa, hata kila mmoja atakayesikia habari zake, atapigwa na bumbuazi. Kwa maana watu wameniacha mimi na kupatia unajisi mahali hapa kwa kufukizia ubani miungu mingine; miungu ambayo wao wenyewe, wazee wao wala wafalme wa Yuda hawajapata kuijua. Pia wamepajaza mahali hapa damu ya watu wasio na hatia, wakamjengea mungu Baali madhabahu, ili kuwachoma wana wao kama sadaka ya kuteketezwa. Mimi sijapata kuamuru wala kuagiza jambo kama hilo lifanywe, wala hata sijapata kulifikiria. Kwa hiyo, jueni kuwa siku zaja ambapo mahali hapa hapataitwa tena Tofethi, wala bonde la Mwana wa Hinomu, bali pataitwa bonde la Mauaji. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Na papa hapa nitaivuruga mipango ya Yuda na Yerusalemu. Nitawafanya watu wao washindwe na kuuawa na maadui zao vitani na kuangamizwa na wale wanaowawinda. Maiti zao nitawaachia ndege wa anga na wanyama wa porini kuwa chakula chao. Nitaufanya mji huu kuwa mahali pa kushangaza; naam, nitaufanya uwe kitu cha kuzomewa. Kila mtu anayepita karibu nao atashangaa na kuuzomea kwa sababu ya maafa yote yatakayoupata. Maadui watauzingira na kujaribu kuwaua watu wake. Watasababisha hali mbaya sana mjini humo hata watu watawala watoto wao wa kike na wa kiume, na kila mtu atamla mwenzake. Kisha wewe utalivunja gudulia hilo mbele ya watu hao watakaokwenda pamoja nawe, na kuwaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nasema hivi: Ndivyo nitakavyovunjavunja watu hawa na mji huu kama vile mtu avunjavyo chombo cha mfinyanzi, hata kisiweze kamwe kutengenezwa tena. Watu watazikwa Tofethi, kwa sababu hapatakuwa na mahali pengine pa kuzikia. Hivyo ndivyo nitakavyopatenda mahali hapa na wakazi wake; nitaufanya mji huu kama Tofethi. Nyumba za Yerusalemu na ikulu za wafalme wa Yuda, naam, nyumba zote ambazo juu ya paa zake watu walifukiza ubani kwa sayari za mbinguni, na kumiminia miungu mingine tambiko za divai, zote zitatiwa unajisi kama Tofethi.” Baada ya hayo, Yeremia aliondoka Tofethi, mahali ambako Mwenyezi-Mungu alimtuma aende kutoa unabii, akaenda na kusimama katika ukumbi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akawatangazia watu wote akisema: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Tazama, mimi nitauletea mji huu na vijiji vyote vilivyo jirani maafa yote niliyoutangazia, kwa sababu wakazi wake ni wakaidi na wamekataa kusikia maneno yangu.” Kuhani Pashuri mwana wa Imeri, ambaye alikuwa ofisa mkuu wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alimsikia Yeremia akitoa unabii huo. Basi, Pashuri akampiga nabii Yeremia na kumtia kifungoni upande wa lango la juu la Benyamini, katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kesho yake asubuhi, Pashuri alipomtoa Yeremia katika mkatale huo, Yeremia alimwambia hivi: “Mwenyezi-Mungu hakuiti tena Pashuri, bali ‘Kitisho Pande Zote’. Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Tazama, nitakufanya uwe kitisho kwako wewe mwenyewe na kwa rafiki zako wote. Wao watauawa vitani kwa upanga wa maadui zao huku ukiangalia. Nitawatia watu wote wa Yuda mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atawachukua mateka hadi Babuloni na kuwaua kwa upanga. Zaidi ya hayo, utajiri wote wa mji, mapato yake yote, vitu vyake vyote vya thamani pamoja na hazina zote za wafalme wa Yuda, nitazitia mikononi mwa maadui zao ambao watazipora na kuchukua kila kitu hadi Babuloni. Na kwa upande wako wewe Pashuri, pamoja na nyumba yako yote, mtapelekwa utumwani; hakika mtakwenda Babuloni. Huko ndiko utakakofia na kuzikwa, kadhalika na rafiki zako wote ambao uliwatabiria uongo.’” Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenidanganya, nami kweli nikadanganyika; wewe una nguvu kuliko mimi, nawe umeshinda. Kutwa nzima nimekuwa mtu wa kuchekwa, kila mtu ananidhihaki. Kila ninaposema kitu, nalalamika, napaza sauti, “Ukatili na uharibifu!” Maana kwangu kutangaza neno la Mwenyezi-Mungu kwanifanya nishutumiwe na kudhihakiwa kutwa nzima. Lakini nikisema, “Sitamtaja Mwenyezi-Mungu, wala sitasema tena kwa jina lake,” moyoni mwangu huwa na kitu kama moto uwakao, uliofungiwa ndani ya mifupa yangu. Najaribu sana kuuzuia humo, lakini ninashindwa. Nasikia wengi wakinongona juu yangu. Wananipanga jina: “Kitisho kila upande!” Wengine wanasema: “Nendeni mkamshtaki! Na tumshtaki!” Hata rafiki zangu wote wapenzi wanangojea tu nianguke! Wanasema “Labda atadanganyika, nasi tutalipiza kisasi.” Lakini wewe Mwenyezi-Mungu u pamoja nami kwangu wewe ni kama shujaa wa kutisha; kwa hiyo watesi wangu watajikwaa, na hawataweza kunishinda. Wataaibika kupindukia, maana hawatafaulu. Fedheha yao itakuwa ya daima; kamwe haitasahaulika. Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, wewe humthibiti mtu mwadilifu, huona yaliyo moyoni na akilini mwa watu, unijalie kuona ukiwalipiza kisasi, maana kwako nimekiweka kisa changu. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu; msifuni Mwenyezi-Mungu, kwani ameyaokoa maisha ya mhitaji, kutoka mikononi mwa watu waovu. Na ilaaniwe siku niliyozaliwa! Siku hiyo mama aliponizaa, isitakiwe baraka! Na alaaniwe aliyempelekea baba ujumbe: “Umepata mtoto wa kiume”, akamfanya ajae furaha. Mtu huyo na awe kama miji aliyoiangusha Mwenyezi-Mungu bila huruma. Mtu huyo na asikie kilio asubuhi, na mchana kelele za vita, kwani hakuniua tumboni mwa mama yangu; mama yangu angekuwa kaburi langu, tumbo lake lingebaki kubwa daima. Kwa nini nilitoka tumboni mwa mama yangu? Je, nilitoka ili nipate taabu na huzuni na kuishi maisha ya aibu? Hili ni neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, wakati mfalme Sedekia alipowatuma Pashuri mwana wa Malkia, na kuhani Sefania mwana wa Maaseya, wamwambie Yeremia hivi: “Tafadhali, tuombee kwa Mwenyezi-Mungu maana Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, anaanza vita dhidi yetu. Labda Mwenyezi-Mungu atatufanyia mwujiza kama afanyavyo mara kwa mara na kumfanya Nebukadneza atuache na kwenda zake.” Yeremia akawaambia: Nendeni mkamwambie Sedekia kwamba hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: “Sedekia! Nitakugeuzia wewe mwenyewe silaha unazotumia kupigana na mfalme wa Babuloni na Wakaldayo wanaowazingira nje ya kuta za mji. Nitazikusanya silaha zote katikati ya mji huu. Mimi mwenyewe nitapigana nawe kwa mkono ulionyoka na wenye nguvu, kwa hasira, ukali na ghadhabu kubwa. Nitawaua wakazi wa mji huu: Binadamu na wanyama kadhalika. Watakufa kwa maradhi mabaya sana. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kuwa, baadaye wewe Sedekia mfalme wa Yuda, watumishi wako na watu wa mji huu ambao mtaponea maradhi hayo mabaya pamoja na vita na njaa, nitawatia mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni na mikononi mwa adui zenu wanaowawinda. Nebukadneza atawaua kwa upanga na wala hatawahurumia au kuwaachilia au kuwasamehe. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nawe Yeremia utawaambia watu hawa kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Sikilizeni! Mimi nawapeni nafasi ya kuchagua njia ya uhai au njia ya kifo. Mtu atakayebaki mjini humu atauawa kwa upanga au kwa njaa au kwa maradhi mabaya. Lakini mtu atakayetoka nje ya mji na kujisalimisha kwa Wakaldayo wanaouzingira mji, ataishi; naam, atayanusurisha maisha yake. Nimeamua kuuletea mji huu maafa na sio mema, nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Nitautia mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atauteketeza kwa moto. “Utaiambia jamaa ya mfalme wa Yuda: Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi jamaa ya Daudi! Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tekelezeni haki tangu asubuhi, na kuwakomboa mikononi mwa wadhalimu wote walionyanganywa mali zao. La sivyo, hasira yangu itachomoza kama moto, itawaka na wala hakuna atakayeweza kuizima, kwa sababu ya matendo yenu maovu. Tazama, mimi sasa napambana nanyi mnaoishi bondeni, mnaokaa kwenye mwamba wa tambarare, nyinyi mnaosema, ‘Nani atathubutu kutushambulia? Nani awezaye kuingia katika makazi yetu?’ Nitawaadhibu kadiri ya matendo yenu; mimi Mwenyezi-Mungu nasema. Nitawasha moto katika msitu wenu nao utateketeza kila kitu kinachouzunguka.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nenda katika ikulu ya mfalme wa Yuda, uwape watu ujumbe huu: Wewe mfalme wa Yuda unayekikalia kiti cha enzi cha mfalme Daudi, pamoja na watumishi wako na watu wako wanaopita katika malango haya, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tendeni mambo ya haki na uadilifu. Mwokoeni mikononi mwa mdhalimu mtu yeyote aliyenyanganywa mali zake. Msiwatendee vibaya au ukatili wageni, yatima na wajane wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia mahali hapa. Kama mkishika neno hili nililowaambia basi, wafalme wanaokikalia kiti cha enzi cha Daudi wataendelea kuingia kwa kupitia malango ya ikulu hii. Watapita pamoja na watumishi wao na watu wao, wakiwa wamepanda farasi na magari ya farasi. Lakini kama hamtatii maneno haya, mimi Mwenyezi-Mungu naapa kwa nafsi yangu kwamba mahali hapa patakuwa magofu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi kuhusu ikulu ya mfalme wa Yuda: “Ingawa waonekana kuwa mzuri kama nchi ya Gileadi kama kilele cha Lebanoni, Lakini naapa kuwa nitakufanya uwe jangwa, uwe mji usiokaliwa na watu. Nitawatayarisha waangamizi dhidi yako, kila mmoja na silaha yake mkononi. Wataikata mierezi yako mizuri, na kuitumbukiza motoni. “Kisha watu wengi wa mataifa watapita karibu na mji huu, na kila mmoja atamwuliza mwenzake: ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ameutenda hivi mji huu mkubwa?’ Wenzao watawajibu, ‘Ni kwa sababu waliliacha agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakaiabudu miungu mingine na kuitumikia.’” Msimlilie mtu aliyekufa, wala msiombolezee kifo chake. Bali mlilieni kwa uchungu yule aendaye mbali, kwa kuwa hatarudi tena kuiona nchi yake. Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Shalumu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, aliyetawala baada ya Yosia baba yake, na ambaye aliondoka mahali hapa: “Shalumu hatarudi tena mahali hapa, bali atafia hukohuko walikomchukua utumwani. Kamwe hataiona tena nchi hii. “Ole wako Yehoyakimu wewe unayejenga nyumba kwa dhuluma na kuiwekea ghorofa bila kutumia haki. Unawaajiri watu wakutumikie bure wala huwalipi mishahara yao. Wewe wasema: ‘Nitalijenga jumba kubwa, lenye vyumba vikubwa ghorofani.’ Kisha huifanyia madirisha, ukafunika kuta zake kwa mbao za mierezi, na kuipaka rangi nyekundu! Unadhani umekuwa mfalme kwa kushindana kujenga kwa mierezi? Baba yako alikula na kunywa, akatenda mambo ya haki na mema ndipo mambo yake yakamwendea vema. Aliwapatia haki maskini na wahitaji, na mambo yake yakamwendea vema. Hii ndiyo maana ya kunijua mimi Mwenyezi-Mungu. Lakini macho yako wewe na moyo wako, hungangania tu mapato yasiyo halali. Unamwaga damu ya wasio na hatia, na kuwatendea watu dhuluma na ukatili. “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu ya Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda: Wakati atakapokufa, hakuna atakayemwombolezea akisema, ‘Ole, kaka yangu!’ ‘Ole, dada yangu!’ Hakuna atakayemlilia akisema, ‘Maskini, bwana wangu!’ ‘Maskini, mfalme wangu!’ Atazikwa bila heshima kama punda, ataburutwa na kutupiliwa mbali, nje ya malango ya Yerusalemu.” Enyi watu wa Yerusalemu, pandeni Lebanoni mpige kelele, pazeni sauti zenu huko Bashani; lieni kutoka milima ya Abarimu, maana wapenzi wenu wote wameangamizwa. Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi mlipokuwa na fanaka, lakini nyinyi mkasema, “Hatutasikiliza.” Hii ndiyo tabia yenu tangu ujana wenu, hamjapata kuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu. Viongozi wenu watapeperushwa na upepo, wapenzi wenu watachukuliwa uhamishoni. Ndipo mtakapoona haya na kufadhaika, kwa sababu ya uovu wenu wote mliotenda. Enyi wakazi wote wa Lebanoni, nyinyi mkaao salama kati ya mierezi; jinsi gani mtakavyopiga kite uchungu utakapowakumba, uchungu kama wa mama anayejifungua! Na kuhusu Konia mfalme wa Yuda, mwanawe Yehoyakimu, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Naapa kwa nafsi yangu mimi Mwenyezi-Mungu kwamba hata kama wewe Konia mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yangu ya mhuri katika mkono wangu wa kulia, ningekuvulia mbali. Nitakutia mikononi mwa wale wanaotaka kuyamaliza maisha yako; naam, mikononi mwa wale unaowaogopa, mikononi mwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni; naam, mikononi mwa Wakaldayo. Nitakufukuzia mbali katika nchi ya kigeni, wewe pamoja na mama yako mzazi. Mtakuwa watumwa katika nchi hiyo ambamo nyote wawili hamkuzaliwa, nanyi mtafia hukohuko. Mtatamani kwa hamu kubwa kurudi katika nchi hii, lakini hamtarudi kamwe. Je, huyu mtu Konia, amekuwa kama chungu kilichovunjika, ambacho hudharauliwa na kutupwa nje? Kwa nini yeye na watoto wake wametupwa mbali wakatupwa katika nchi wasiyoijua? Ee nchi, ee nchi, ee nchi! Sikia neno la Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu asema hivi: Mwandike mtu huyu kwamba hana watoto, mtu ambaye hatafanikiwa maishani mwake. Maana hakuna hata mmoja wa wazawa wake atakayekikalia kiti cha enzi cha Daudi na kutawala tena katika Yuda. “Ole wao wachungaji wanaowaangamiza na kuwatawanya kondoo wa malisho yangu!” Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli nasema hivi kuhusu wachungaji wanaowachunga watu wangu: Nyinyi mmewatawanya kondoo wangu na kuwafukuza, wala hamkuwatunza. Basi, nami pia nitawaadhibu kwa ajili ya matendo yenu maovu. Kisha, nitawakusanya kondoo wangu waliobaki kutoka nchi zote nilikowatawanya, na kuwarudisha malishoni mwao. Nao watazaa na kuongezeka. Nitawapa wachungaji watakaowatunza vema, nao hawatakuwa na woga tena wala kufadhaika, na hakuna hata mmoja wao atakayepotea, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Tazama, siku zaja nitakapomchipushia Daudi chipukizi adili. Huyo atatawala kama mfalme, na atatenda kwa busara, haki na uadilifu katika nchi. Katika siku za utawala wake, Yuda ataokolewa na Israeli ataishi kwa usalama. Naye ataitwa, ‘Mwenyezi-Mungu ni uadilifu wetu.’ “Kwa hiyo siku zaja, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, ambapo watu hawataapa tena kwa kusema, ‘Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu aliyewatoa watu wa Israeli nchini Misri’, bali wataapa kwa kusema, ‘Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu aliyewatoa na kuwaongoza Waisraeli kutoka nchi ya kaskazini na kutoka nchi zote ambako aliwatawanya.’ Kisha wataishi katika nchi yao wenyewe.” Kuhusu hao manabii wasiofaa, mimi imevunjika moyo, mifupa yangu yote inatetemeka; nimekuwa kama mlevi, kama mtu aliyelemewa na pombe, kwa sababu yake Mwenyezi-Mungu na maneno yake matakatifu. Maana, nchi imejaa wazinzi; kwa sababu ya laana, nchi inaomboleza, na malisho ya nyanda zake yamekauka. Mienendo ya watu ni miovu, nguvu zao zinatumika isivyo halali. Mwenyezi-Mungu asema: “Manabii na makuhani, wote hawamchi Mungu, uovu wao nimeuona hata nyumbani mwangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Kwa hiyo njia zao zitakuwa vichochoro vya utelezi gizani ambamo watasukumwa na kuanguka; maana, nitawaletea maafa, ufikapo mwaka wa kuwaadhibu, Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Miongoni mwa manabii wa Samaria, nimeona jambo la kuchukiza sana: Walitabiri kwa jina la Baali wakawapotosha watu wangu Waisraeli. Lakini miongoni mwa manabii wa Yerusalemu, nimeona kinyaa cha kutisha zaidi: Wanafanya uzinzi na kusema uongo; wanawaunga mkono wanaotenda maovu hata pasiwe na mtu anayeachana na uovu. Kwangu wote wamekuwa kama watu wa Sodoma; wakazi wake wamekuwa wabaya kama watu wa Gomora. “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi juu ya manabii wa Yerusalemu: Nitawalisha uchungu, na kuwapa maji yenye sumu wanywe. Maana, kutoka kwa manabii wa Yerusalemu kutomcha Mungu kumeenea kila mahali nchini.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Msisikilize maneno ya manabii wanaowatabiria; wanawapeni matumaini ya uongo. Wanayowaambia ni maono yao wenyewe, wala hayakutoka kwangu mimi Mwenyezi-Mungu. Wao hawakomi kuwaambia wale wanaodharau neno langu mimi Mwenyezi-Mungu: ‘Mambo yatawaendea vema.’ Na kumwambia kila mtu afuataye kwa ukaidi fikira zake; ‘Hakuna baya lolote litakalokupata!’” Lakini, ni yupi kati ya manabii hao aliyepata kuhudhuria baraza la Mwenyezi-Mungu, hata akasikia na kuelewa neno lake? Au ni nani aliyejali neno lake, hata akapata kulitangaza? Tazama, dhoruba kutoka kwa Mwenyezi-Mungu! Ghadhabu imezuka; kimbunga cha tufani kitamlipukia mtu mwovu kichwani. Hasira ya Mwenyezi-Mungu haitarudi nyuma, mpaka atakapotekeleza na kukamilisha matakwa ya moyo wake. Siku zijazo mtayaelewa vema mambo hayo. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi sikuwatuma hao manabii, lakini wao walikwenda mbio; sikuwaambia kitu chochote, lakini wao walitabiri! Kama wangalihudhuria baraza langu, wangaliwatangazia watu wangu maneno yangu, wakawageuza kutoka katika njia zao mbovu, na kutoka katika matendo yao maovu. “Mimi ni Mungu aliye karibu, si Mungu aliye mbali. Je, mtu aweza kujificha mahali pa siri hata nisiweze kumwona? Hamjui kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nipo kila mahali, mbinguni na duniani? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mimi nimeyasikia maneno waliyosema hao manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, ‘Nimeota ndoto, nimeota ndoto!’ Itakuwa hivyo mpaka lini? Hao manabii wataendelea mpaka lini kupotoka moyo; kutabiri uongo na udanganyifu wa mioyo yao wenyewe? Kwa ndoto zao hizo wanapanga kuwafanya watu wangu wanisahau mimi kama baba zao walivyonisahau, wakamwendea Baali! Nabii aliyeota ndoto, na aitangaze ndoto yake, lakini yeye aliye na neno langu, na alitangaze kwa uaminifu. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema, makapi si sawa na ngano! Neno langu ni kama moto; ni kama nyundo ipasuayo miamba vipandevipande. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nitawashambulia manabii ambao wanaibiana maneno yangu. Kweli mimi Mwenyezi-Mungu nasema, nitawashambulia manabii wanaoropoka maneno yao wenyewe na kusema, ‘Mwenyezi-Mungu asema’. Naam, mimi Mwenyezi-Mungu nasema kuwa nitawashambulia manabii wanaotabiri ndoto zao za uongo kwa watu wangu, na kuwapotosha kwa uongo wao na kuropoka kwao. Mimi sikuwatuma wala kuwaamuru waende; kwa hiyo hawatawafaa watu hao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Mtu yeyote, awe nabii au kuhani, akikuuliza: ‘Uko wapi mzigo anaotubebesha Mwenyezi-Mungu?’ Wewe utawaambia: ‘Nyinyi ndio mzigo kwa Mwenyezi-Mungu naye atawatupa mbali.’ Tena nabii au kuhani, au mtu yeyote atakayesema ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ nitamwadhibu pamoja na jamaa yake yote. Kitu mnachopaswa kuulizana nyinyi kwa nyinyi ni ‘Mwenyezi-Mungu amejibu nini?’ au, ‘Mwenyezi-Mungu amesema nini?’ Lakini jambo la ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ msilitaje tena. Kile anachosema binadamu ni mzigo kwake mwenyewe. Watu wanayapotosha maneno ya Mungu aliye hai, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao. Basi mtamwuliza nabii hivi: ‘Mwenyezi-Mungu amekujibu nini?’ au, ‘Mwenyezi-Mungu amesema nini?’ Lakini wao wakivunja amri yangu na kusema, ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ wakati ambapo mimi niliwakataza wasiseme, ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ basi, waambie kuwa mimi nitawanyanyua na kuwatupilia mbali, wao wenyewe pamoja na mji niliowapa wao na wazee wao. Nitawaletea fedheha ya milele na aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.” Baada ya Nebukadneza, mfalme wa Babuloni kuwahamisha Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na viongozi wa Yuda, mafundi stadi na masonara, kutoka Yerusalemu na kuwapeleka Babuloni, Mwenyezi-Mungu alinionesha ono hili: Niliona vikapu viwili vya tini vimewekwa mbele ya hekalu la Mwenyezi-Mungu. Kikapu cha kwanza kilikuwa na tini nzuri sana, kama tini za mwanzo wa mavuno. Lakini kikapu cha pili kilikuwa na tini mbaya sana, mbaya hata hazifai kuliwa. Basi, Mwenyezi-Mungu akaniuliza: “Yeremia! Unaona nini?” Mimi nikamjibu: “Naona tini. Zile nzuri ni nzuri sana, na zile mbaya ni mbaya sana hata hazifai kuliwa.” Hapo neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Basi, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Kama tini hizi zilivyo nzuri, ndivyo nitakavyowaona kuwa wema watu wa Yuda ambao niliwatoa mahali hapa na kuwapeleka uhamishoni katika nchi ya Wakaldayo. Nitawalinda daima na kuwarudisha katika nchi hii. Nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawapanda, wala sitawangoa. Nitawapa moyo wa kujua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao; maana watanirudia kwa moyo wao wote. “Lakini mimi Mwenyezi-Mungu nasema: Kama tini zile mbaya, tini zilizo mbaya hata hazifai kuliwa, ndivyo nitakavyowatenda mfalme Sedekia wa Yuda, maofisa wake pamoja na watu wengine wote wa Yerusalemu waliobaki nchini humo, kadhalika na wale ambao walihamia nchini Misri. Nitawafanya kuwa kitu cha kuchukiza mbele ya falme zote duniani. Watakuwa kitu cha dhihaka, kitu cha kuzomewa, kuchekwa na kulaaniwa kila mahali nitakapowafukuzia. Nao nitawaletea vita, njaa na maradhi mabaya mpaka waangamizwe kabisa kutoka katika nchi niliyowapa wao na wazee wao.” Mnamo mwaka wa nne wa utawala wa mfalme Yehoyakimu mwana wa Yosia, katika Yuda, Mwenyezi-Mungu alinimpa mimi Yeremia ujumbe kuhusu watu wa Yuda. Mwaka huo ulikuwa wa kwanza wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babuloni. Mimi Yeremia niliwaambia ujumbe huo watu wote wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu: “Kwa muda wa miaka ishirini na mitatu sasa, yaani tangu mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa mfalme Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, mpaka hivi leo, nimekuwa nikipata neno la Mungu na kuwaambieni kila wakati, lakini nyinyi hamkusikiliza. Hamkutaka kusikiliza wala hamkutega sikio msikie, ingawa Mwenyezi-Mungu aliwaleteeni watumishi wake manabii kila wakati, wakawaambieni kwamba kila mmoja wenu aachane na mwenendo wake mwovu na matendo yake mabaya, ili mpate kuishi katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu amewapa nyinyi na wazee wenu tangu zamani, muimiliki milele. Mwenyezi-Mungu aliwaonya Mmsifuate miungu mingine wala kuitumikia na kumkasirisha Mungu kwa kuabudu sanamu ambazo mmejitengenezea wenyewe. Kama Mmkimtii Mwenyezi-Mungu basi, yeye hatawaadhibu. Lakini Mwenyezi-Mungu asema kuwa nyinyi mlikataa kumsikiliza. Badala yake, mlimkasirisha kwa sanamu mlizojitengenezea wenyewe, na hivyo mkajiletea madhara nyinyi wenyewe. “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: “Kwa kuwa hamkuyatii maneno yangu, basi, nitayaita makabila yote ya kaskazini, pamoja na mtumishi wangu Nebukadneza, mfalme wa Babuloni. Nitawaleta waishambulie nchi hii na wakazi wake pamoja na mataifa yote ya jirani. Nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kuwa kitu cha kuchukiza, kuzomewa na kudharauliwa milele. Tena, nitakomesha miongoni mwao sauti za furaha, sauti za bwana arusi na bibi arusi. Sauti za kusaga hazitakuwapo, wala mwanga wa taa. Nchi hii yote itakuwa magofu matupu na ukiwa, na mataifa ya jirani yatamtumikia mfalme wa Babuloni kwa muda wa miaka sabini. Kisha baada ya miaka hiyo sabini kukamilika nitamwadhibu mfalme wa Babuloni pamoja na taifa hilo. Nitaiangamiza nchi hiyo ya Wakaldayo kwa sababu ya uovu wao na kuifanya nchi iwe magofu milele. Nitailetea nchi hiyo mambo yote niliyotamka dhidi yake na yote yaliyoandikwa katika kitabu hiki ambayo Yeremia alitabiri dhidi ya mataifa yote. Wababuloni nao itawalazimu kuwa watumwa wa mataifa mengine na wafalme wengine. Nitawaadhibu kadiri ya maovu yao waliyotenda.” Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliniambia hivi: “Chukua mkononi mwangu hiki kikombe cha divai ya ghadhabu yangu uyanyweshe mataifa yote ninayokutuma kwao. Mataifa hayo yatakunywa na kupepesuka na kurukwa na akili kwa sababu ya mauaji nitakayosababisha kati yao.” Basi, nikachukua hicho kikombe mkononi mwa Mwenyezi-Mungu, nikayanywesha mataifa yote ambayo Mwenyezi-Mungu alinituma kwao. Kwanza Yerusalemu na miji ya Yuda, wafalme wake na viongozi wake, ili kuifanya iwe jangwa, ukiwa, kitu cha kuzomewa na kulaaniwa, kama ilivyo mpaka leo. Halafu: Farao, mfalme wa Misri, maofisa na viongozi wake, pamoja na watu wake wote; wageni wote walioishi nchini Misri; wafalme wote wa nchi ya Uzi; wafalme wote wa miji ya Wafilisti, Ashkeloni, Gaza, Ekroni na mabaki ya Ashdodi. Watu wote wa Edomu, Moabu na Amoni; wafalme wote wa Tiro na Sidoni; wafalme wa nchi za pwani ya bahari ya Mediteranea; wakazi wa Dedani, Tema, Buzi na watu wote wanyoao denge; wafalme wote wa Arabia; wafalme wote wa makabila yaliyochanganyika jangwani; wafalme wote wa Zimri, Elamu na Media; wafalme wote wa kaskazini, mbali na karibu, mmoja baada ya mwingine. Falme zote ulimwenguni zitakunywa. Na, baada ya hao wote naye mfalme wa Babuloni atakunywa. Mwenyezi-Mungu akaniamuru: “Utawaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Kunyweni, mlewe na kutapika; angukeni wala msiinuke tena, kwa sababu ya mauaji ninayosababisha miongoni mwenu. Kama wakikataa kukipokea kikombe hicho mkononi mwako na kunywa, wewe utawaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nasema kwamba ni lazima wanywe! Tazama! Sasa ninaanza kuleta maafa katika mji unaoitwa kwa jina langu; je, mnadhani mnaweza kuepukana na adhabu? Hamtaachwa bila kuadhibiwa, maana ninaleta mauaji dhidi ya wakazi wote wa dunia. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. “Basi, wewe Yeremia utatabiri maneno haya yote dhidi yao, na kusema hivi: Mwenyezi-Mungu atanguruma kutoka juu, atatoa sauti yake kutoka makao yake matakatifu; atanguruma kwa nguvu dhidi ya watu wake, na kupaza sauti kama wenye kusindika zabibu, dhidi ya wakazi wote wa dunia. Vishindo hivyo vitasikika hadi mwisho wa dunia, maana Mwenyezi-Mungu ana mashtaka dhidi ya mataifa; anawahukumu wanadamu wote, na waovu atawaua kwa upanga! Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Tazama, maafa yatalikumba taifa moja baada ya lingine, na tufani itazuka kutoka miisho ya dunia.” Siku hiyo, watakaouawa na Mwenyezi-Mungu watatapakaa kutoka upande mmoja wa dunia hadi mwingine. Hawataombolezewa, hawatakusanywa wala kuzikwa; watabaki kuwa mavi juu ya ardhi. Ombolezeni enyi wachungaji; lieni na kugaagaa majivuni enyi wakuu wa kundi; siku za kuchinjwa kwenu na kutawanywa zimefika; mtauawa kama kondoo madume waliochaguliwa. Wachungaji hawatakuwa na pa kukimbilia, wala wakuu wa kundi hawataweza kutoroka. Sikilizeni kilio cha wachungaji na mayowe ya wakuu wa kundi! Mwenyezi-Mungu anayaharibu malisho yao, na makundi yaliyokuwa matulivu yameharibiwa kwa sababu ya hasira kali ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu amewaacha watu wake, kama vile simba aachavyo pango lake; nchi yao imekuwa jangwa tupu, kwa sababu ya vita vya wadhalimu, na hasira kali ya Mwenyezi-Mungu. Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia, katika nchi ya Yuda, Mwenyezi-Mungu alimwambia Yeremia hivi: “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Simama katika ukumbi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, uwatangazie watu wa miji yote ya Yuda wanaofika kuabudu katika nyumba ya Mungu, mambo yote niliyokuamuru uwaambie, bila kuacha hata neno moja. Labda watasikiliza na kuacha njia zao mbaya. Wakifanya hivyo, huenda nikabadili nia yangu kuhusu maafa niliyonuia kuwaletea kwa sababu ya matendo yao maovu. “Utawaambia hivi: Mwenyezi-Mungu asema hivi: Msiponisikiliza na kufuata sheria zangu nilizowawekea, na msipoyajali wanayosema watumishi wangu manabii ambao nimekuwa nikiwatuma kwenu kila mara, ingawa hamkuwajali, basi, nitaiharibu nyumba hii kama nilivyoharibu ile ya Shilo, na nitaufanya mji huu kuwa laana kwa mataifa yote ya dunia.” Makuhani, manabii na watu wote walimsikia Yeremia akisema maneno haya katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Basi Yeremia alipomaliza kutangaza mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimwamuru ayatangaze kwa watu wote, makuhani, manabii na watu wote walimkamata na kusema, “Utakufa! Kwa nini umetabiri kwa jina la Mwenyezi-Mungu na kusema, nyumba hii itakuwa kama Shilo na mji huu utakuwa ukiwa, bila wakazi?” Watu wote wakamzingira Yeremia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Basi, wakuu wa Yuda waliposikia mambo hayo, walipanda kutoka katika nyumba ya mfalme, wakaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaketi penye Lango Jipya. Hapo makuhani na manabii wakawaambia wakuu na watu wote: “Mtu huyu anastahili hukumu ya kifo kwa maana amehubiri dhidi ya mji huu, kama nyinyi wenyewe mlivyosikia kwa masikio yenu.” Ndipo Yeremia akawaambia wakuu na watu wote: “Mwenyezi-Mungu alinituma niwatabirie mambo yote mliyosikia nikiyasema dhidi ya hekalu hili na mji huu. Sasa basi, rekebisheni mienendo yenu na matendo yenu na kutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mkifanya hivyo, Mwenyezi-Mungu atabadili nia yake na kuacha kuwaletea maafa aliyotamka dhidi yenu. Lakini mimi, tazama nimo mikononi mwenu. Nitendeeni kama mnavyoona vema na haki. Ila jueni kwa hakika kwamba mkiniua, mtakuwa mmejiletea laana nyinyi wenyewe kwa kumwaga damu isiyo na hatia, na kuuletea laana mji huu na wakazi wake. Maana, ni kweli kwamba Mwenyezi-Mungu alinituma niwaambieni mambo hayo muyasikie.” Hapo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani na manabii: “Mtu huyu hastahili hukumu ya kifo, kwa kuwa amesema nasi kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.” Basi, baadhi ya wazee wa nchi wakasimama na kuwaambia watu waliokuwa wamekusanyika: “Wakati Hezekia alipokuwa mfalme wa Yuda, Mika wa Moreshethi, aliwatangazia watu wote kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi alisema hivi: ‘Mji wa Siyoni utalimwa kama shamba mji wa Yerusalemu utakuwa magofu, nao mlima wa hekalu utakuwa msitu.’ Je, Hezekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa Yuda walimuua Mika? La! Badala yake Hezekia alimwogopa Mwenyezi-Mungu na kuomba fadhili zake. Naye Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake ya kuwaletea balaa. Lakini sisi tuko mbioni kujiletea wenyewe maafa.” (Kulikuwa na mtu mwingine pia aliyetabiri kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo alikuwa anaitwa Uria mwana wa Shemaya, kutoka mji wa Kiriath-yearimu. Yeye alitabiri dhidi ya mji huu na dhidi ya nchi hii kama alivyofanya Yeremia. Naye mfalme Yehoyakimu pamoja na mashujaa wake na wakuu wote waliposikia mambo aliyosema Uria, mfalme alitaka kumuua. Lakini Uria alipopata habari, alishikwa na hofu, akatoroka na kwenda Misri. Mfalme Yehoyakimu alimpeleka Elnathani mwana wa Akbori, pamoja na watu kadhaa huko Misri. Wao walimrudisha Uria kutoka Misri, wakampeleka kwa mfalme Yehoyakimu. Mfalme akamuua kwa upanga na maiti yake ikazikwa kwenye makaburi ya watu wa kawaida.) Lakini Yeremia alikuwa akilindwa na Ahikamu mwana wa Shefani, ili asitiwe mikononi mwa watu na kuuawa. Mwanzoni mwa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Yeremia, jitengenezee kamba na nira ujivike shingoni. Kisha, peleka ujumbe kwa mfalme wa Edomu, mfalme wa Moabu, mfalme wa Amoni, mfalme wa Tiro na mfalme wa Sidoni, kupitia kwa wajumbe waliokuja Yerusalemu kumwona Sedekia mfalme wa Yuda. Waamuru wajumbe hao wawaambie wakuu wao kwamba mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Mimi ndimi niliyeiumba dunia, watu na wanyama waliomo kwa uwezo wangu na kwa mkono wangu wenye nguvu, nami humpa mtu yeyote kama nionavyo mimi kuwa sawa. Sasa nimemkabidhi mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babuloni, nchi hizi zote; kadhalika nimempa wanyama wa porini wamtumikie. Mataifa yote yatamtumikia yeye, mwanawe na mjukuu wake, mpaka wakati nchi yake itakapoanguka. Kisha mataifa mengi na wafalme wengi watamfanya kuwa mtumwa wao. “Lakini kama taifa lolote au utawala wowote hautajiweka chini ya mamlaka ya Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, basi, nitaliadhibu taifa hilo kwa vita, njaa na maradhi mpaka niliangamize kabisa kwa mkono wake. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Basi, nyinyi msiwasikilize manabii wenu, wapiga ramli wenu, watabiri wenu, waaguzi wenu au wachawi wenu, wanaowaambia: ‘Msimtii mfalme wa Babuloni.’ Hao wanawatabirieni uongo na hii itasababisha mhamishwe mbali na nchi yenu. Nitawafukuzia mbali, nanyi mtaangamia. Lakini watu wa taifa lolote litakalomtii mfalme wa Babuloni na kumtumikia, nitawaacha wakae nchini mwao, wailime ardhi yao na kuishi humo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mimi Yeremia nilikuwa nimemwambia Sedekia mfalme wa Yuda, mambo hayohayo. Nilimwambia: “Mtii mfalme wa Babuloni. Mtumikie yeye na watu wake, nawe utaishi. Ya nini wewe na watu wako kufa kwa vita, njaa na maradhi? Maana, hivyo ndivyo alivyosema Mwenyezi-Mungu kuhusu yatakayolipata taifa lolote litakaloacha kumtumikia mfalme wa Babuloni. Usisikilize maneno ya manabii wanaokuambia: ‘Usimtumikie mfalme wa Babuloni’, kwa sababu wanakutabiria uongo. Mwenyezi-Mungu anasema: ‘Mimi sikuwatuma manabii hao, bali wanatabiri uongo kwa jina langu. Kwa hiyo nitawafukuzia mbali, nanyi mtaangamia, pamoja na hao manabii wanaowatabirieni uongo.’” Kisha, niliwaambia makuhani na watu wote: Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Msiwasikilize manabii wenu wanaowatabiria wakisema: ‘Tazama, vyombo vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu vitarudishwa hivi karibuni kutoka Babuloni’, kwa maana wanawadanganyeni. Msiwasikilize. Mtumikieni mfalme wa Babuloni, nanyi mtaishi. Ya nini mji huu ufanywe kuwa magofu? Ikiwa wao ni manabii, na kama wana neno la Mwenyezi-Mungu, basi, na wamsihi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ili vyombo vilivyobaki katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika nyumba ya mfalme wa Yuda, na katika mji wa Yerusalemu, visichukuliwe na kupelekwa Babuloni. Kwa maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi juu ya nguzo, sinia za shaba, vinara na vyombo vingine vilivyoachwa katika mji huu ambavyo Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, hakuvichukua wakati alipowachukua Yekonia mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda na waheshimiwa wote wa Yuda na Yerusalemu kutoka Yerusalemu na kuwapeleka uhamishoni. “Sikilizeni mambo ambayo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, ninasema juu ya vile vyombo vilivyoachwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, katika nyumba ya mfalme wa Yuda na katika mji wa Yerusalemu. Vyombo hivyo vitachukuliwa Babuloni na vitabaki huko mpaka siku nitakapovishughulikia. Hapo ndipo nitakapovirudisha na kuviweka tena mahali hapa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwaka uleule, mnamo mwezi wa tano wa mwaka wa nne wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, Hanania mwana wa Azuri, nabii kutoka mji wa Gibeoni, alisema nami katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Alisema nami mbele ya makuhani na watu wote, akaniambia, “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Nimeivunja nira ya mfalme wa Babuloni. Mnamo miaka miwili nitavirudisha hapa vyombo vyote vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambavyo Nebukadneza, mfalme wa Babuloni alivichukua na kuvipeleka Babuloni. Pia nitamrudisha Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na watu wote wa Yuda waliohamishiwa Babuloni. Naam, nitaivunja nira ya mfalme wa Babuloni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Kisha, nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania mbele ya makuhani na watu wote waliokuwa wamesimama katika hekalu la Mwenyezi-Mungu: “Na iwe hivyo! Mwenyezi-Mungu na afanye hivyo. Mwenyezi-Mungu na ayatimize maneno uliyotabiri, avirudishe hapa vyombo vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kutoka Babuloni pamoja na watu wote waliohamishiwa huko. Lakini sikiliza neno ninalokuambia wewe na watu wote. Manabii waliotutangulia mimi na wewe, tangu zamani za kale, walitabiri kwamba vita, njaa na maradhi vitazikumba nchi nyingi na tawala kubwa. Lakini nabii atabiriye amani, hutambuliwa tu kama nabii aliyetumwa na Mwenyezi-Mungu, ikiwa mambo aliyotabiri hutokea kweli.” Ndipo nabii Hanania akaichukua ile nira shingoni mwa nabii Yeremia, akaivunja. Naye Hanania akasema hivi mbele ya watu wote, “Mwenyezi-Mungu asema: Hivi ndivyo nitakavyovunja nira ambayo mfalme Nebukadneza ameyavisha mataifa yote; nitafanya hivyo mnamo miaka miwili ijayo.” Kisha nabii Yeremia akaenda zake. Baada ya nabii Hanania kuvunja nira kutoka shingoni mwa nabii Yeremia, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia: “Nenda ukamwambie Hanania kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe umevunja nira ya mti, lakini mimi nitatengeneza nyingine ya chuma. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema kuwa nimeweka nira ya chuma ya utumwa shingoni mwa mataifa haya yote, nayo yatamtumikia Nebukadneza, mfalme wa Babuloni. Nimempa Nebukadneza hata wanyama wa porini wamtumikie.” Basi, nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, “Sikiliza, Hanania, Mwenyezi-Mungu hakukutuma, nawe unawafanya watu hawa waamini uongo. Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu asema kwamba atakuondoa duniani. Mwaka huuhuu utakufa, kwa sababu umewaambia watu wamwasi Mwenyezi-Mungu.” Mwaka huohuo, mnamo mwezi wa saba, nabii Hanania akafa. Ifuatayo ni barua ambayo nabii Yeremia aliwapelekea kutoka Yerusalemu wazee na makuhani, manabii na watu ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kutoka Yerusalemu akawapeleka uhamishoni Babuloni. Yeremia aliiandika barua hiyo baada ya mfalme Yekonia na mama mfalme, matowashi, wakuu wa Yuda na Yerusalemu, mafundi na wahunzi kuondoka Yerusalemu. Barua hii ilipelekwa na Elasa mwana wa Shafani, na Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma kwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni. Yeremia aliandika hivi: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi kuhusu mateka wote aliowaacha wachukuliwe kutoka Yerusalemu hadi Babuloni: ‘Jengeni nyumba mkae. Limeni mashamba, pandeni mbegu na kula mazao yake. Oeni wake, mpate watoto; waozeni wana wenu na binti zenu nao pia wapate watoto. Ongezekeni na wala msipungue. Shughulikieni ustawi wa mji ambamo nimewahamishia. Niombeni kwa ajili ya mji huo, maana katika ustawi wake nyinyi mtastawi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Msikubali kudanganywa na manabii wenu na waaguzi waliomo miongoni mwenu, wala msisikilize ndoto wanazoota. Maana wanawatabiria uongo kwa kutumia jina langu. Mimi sikuwatuma. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.’ “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Baada ya miaka sabini huko Babuloni, baada ya muda huo, nitawajia na kuitimiza ahadi yangu ya kuwarudisha mahali hapa. Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye. Hapo ndipo mtakaponiita na kuniomba, nami nitawasikiliza. Mtanitafuta na kunipata. Mtakaponitafuta kwa moyo wote mtanipata. Nami nitawarudishieni fanaka zenu na kuwakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipowafukuzia. Nitawarudisheni mahali ambapo niliwatoa, nikawapeleka uhamishoni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nyinyi mnawasadiki manabii ambao mwasema kwamba Mwenyezi-Mungu amewaleteeni huko Babuloni. Sikilizeni nisemavyo mimi Mwenyezi-Mungu kuhusu mfalme anayekalia kiti cha enzi cha Daudi, na kuhusu watu wote wanaokaa katika mji huu, na ndugu zenu ambao hawakuondoka pamoja nanyi kwenda uhamishoni. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Tazama, ninawapelekea upanga, njaa na maradhi mabaya; nitawafanya kuwa kama tini mbaya sana, hata haziwezi kuliwa. Nitawaandama kwa upanga, njaa na maradhi mabaya. Nitawafanya kuwa kitu cha kuchukiza kwa tawala zote za dunia, naam, kitu cha laana, kioja, dharau na kitu cha kupuuzwa katika mataifa yote nilikowafukuzia. Nitafanya hivyo kwa sababu hamkusikiliza maneno yangu niliyowaambia kila mara kwa njia ya watumishi wangu, manabii, nanyi mkakataa kusikiliza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Enyi nyote niliowatoa kutoka Yerusalemu, nikawapeleka uhamishoni Babuloni, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi juu ya Ahabu mwana wa Kolaya, na juu ya Sedekia mwana wa Maaseya, ambao wanawatabirieni uongo kwa jina lake: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, naye atawaua mkiona kwa macho yenu wenyewe. Kwa sababu jambo hilo litakalowapata, watu wote waliohamishiwa Babuloni kutoka Yerusalemu watatumia msemo huu wa kulaania: Mwenyezi-Mungu akufanye kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babuloni aliwachoma motoni. Kisa ni kwamba walitenda mambo ya aibu katika Israeli. Walizini na wake za jirani zao, na kusema maneno ya uongo kwa jina langu, jambo ambalo mimi sikuwaamuru walifanye. Mimi nayajua hayo; nimeyashuhudia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu aliniagiza nimwambie hivi Shemaya wa Nehelamu: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Umepeleka barua kwa jina lako kwa wakazi wote wa Yerusalemu na kwa kuhani Sefania mwana wa Maaseya na kwa makuhani wengine wote. Katika barua hiyo, ulimwambia Sefania hivi: ‘Mwenyezi-Mungu amekufanya wewe Sefania kuwa kuhani badala ya kuhani Yehoyada, uwe mkuu wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Ni wajibu wako kumtia gerezani na kumfunga minyororo mwendawazimu yeyote anayetabiri. Kwa nini basi, hukumkemea Yeremia kutoka Anathothi anayekutabiria? Maana yeye alituma taarifa huko Babuloni kwamba uhamisho wenu utakuwa wa muda mrefu, na kusema mjenge nyumba, mkae; mlime mashamba, mpande mbegu na kula mazao yake!’” Kuhani Sefania aliisoma barua hiyo mbele ya nabii Yeremia. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Yeremia: “Wapelekee watu wote walioko uhamishoni ujumbe huu: Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu ya Shemaya wa Nehelamu: Shemaya amewatabirieni, hali mimi sikumtuma, akawafanya muuamini uongo. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu nasema kuwa nitamwadhibu Shemaya wa Nehelamu pamoja na wazawa wake. Hakuna hata mmoja wa watu wake atakayebaki hai kuona mema nitakayowafanyia watu wangu, kwa sababu amewachochea watu waniasi mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu: “Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Yaandike katika kitabu maneno yote niliyokuambia. Maana siku zaja ambapo nitawarudishia fanaka zao watu wangu wa Israeli na Yuda na kuwarudisha katika nchi niliyowapa wazee wao, nao wataimiliki. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Haya ndiyo mambo aliyosema Mwenyezi-Mungu kuhusu watu wa Israeli na Yuda: “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kumesikika kilio cha hofu sauti ya kutisha wala si ya amani. Jiulizeni sasa na kufahamu: Je, mwanamume aweza kujifungua mtoto? Mbona basi, namwona kila mwanamume amejishika kiunoni kama mwanamke mwenye utungu na nyuso zao zimegeuka rangi? Kweli, siku hiyo ni kubwa, hakuna nyingine kama hiyo; ni siku ya huzuni kwa watu wa Yakobo; hata hivyo, wataokolewa humo. “Siku hiyo itakapofika, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nitaivunja nira iliyo shingoni mwao na kukata minyororo yao. Nao hawatakuwa tena watumwa wa wageni, bali watanitumikia mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, na mfalme wa ukoo wa Daudi ambaye nitawateulia. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Usiogope ee Yakobo mtumishi wangu, wala usifadhaike, ee Israeli; maana nitakuokoa huko mbali uliko, na wazawa wako kutoka uhamishoni. Utarudi na kuishi kwa amani, wala hakuna mtu atakayekuogopesha. Maana mimi niko pamoja nawe, kukuokoa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitayaangamiza kabisa mataifa yote, ambayo nilikutawanya kati yao; lakini wewe sitakuangamiza kabisa. Nitakuadhibu kadiri unavyostahili wala sitakuacha uende bila kukuadhibu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Majeraha yako hayaponyeki, vidonda vyako havitibiki. Hakuna atakayeshughulikia kisa chako, jeraha lako halina dawa, wewe hutaponyeshwa. Wapenzi wako wote wamekusahau; hawajali chochote juu yako, nimekupiga pigo la adui; umeadhibiwa bila huruma, kwa kuwa kosa lako ni kubwa, dhambi zako ni nyingi mno. Mbona unalia juu ya jeraha lako? Maumivu yako hayaponyeki. Nimekutendea hayo yote, kwa sababu kosa lako ni kubwa, dhambi zako ni nyingi mno. Lakini wote wanaokuangamiza, wataangamizwa, na maadui zako wote watachukuliwa uhamishoni; wanaokuteka nyara, watatekwa nyara, wanaokuwinda nitawawinda. “Nitakurudishia afya yako, na madonda yako nitayaponya, japo wamekuita ‘Aliyetupwa’, ‘Mji Siyoni usio na wa kuutunza!’” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nitazirudisha tena fanaka za maskani ya Yakobo, na kuyaonea huruma makao yake; mji utajengwa upya juu ya magofu yake, na ikulu ya mfalme itasimama pale ilipokuwa. Humo zitatoka nyimbo za shukrani na sauti za wale wanaosherehekea. Nitawaongeza na wala hawatakuwa wachache; nitawafanya waheshimiwe wala hawatadharauliwa. Watoto wao watakuwa kama walivyokuwa zamani, jumuiya yao itaimarika mbele yangu, nami nitawaadhibu wote wanaowakandamiza. Kiongozi wao atakuwa mmoja wao, mtawala wao atatokea miongoni mwao. Nitamleta karibu naye atanikaribia; maana, nani anayethubutu kunikaribia kwa nguvu zake? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.” Tazama, dhoruba kali kutoka kwa Mwenyezi-Mungu! Ghadhabu imezuka, kimbunga cha tufani kitamlipukia mtu mwovu kichwani. Hasira ya Mwenyezi-Mungu haitarudi nyuma, mpaka atakapotekeleza na kukamilisha matakwa ya moyo wake. Siku zijazo mtayaelewa vema mambo hayo. Mwenyezi-Mungu asema: “Wakati utakuja ambapo nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli nao watakuwa watu wangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema: Watu walionusurika kuuawa niliwaneemesha jangwani. Wakati Israeli alipotafuta kupumzika, mimi Mwenyezi-Mungu nilimtokea kwa mbali. Nami nimekupenda kwa mapendo ya daima, kwa hiyo nimeendelea kuwa mwaminifu kwako. Nitakujenga upya nawe utajengeka, ewe Israeli uliye mzuri! Utazichukua tena ngoma zako ucheze kwa furaha na shangwe. Utapanda tena mizabibu juu ya milima ya Samaria; wakulima watapanda mbegu na kuyafurahia mazao yake! Maana siku yaja ambapo mlinzi atapiga mbiu katika vilima vya Efraimu: ‘Amkeni, twende juu mpaka Siyoni kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’” Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Imbeni kwa furaha kwa ajili ya Yakobo, pigeni vigelegele kwa ajili ya taifa kuu, tangazeni, shangilieni na kusema: ‘Mwenyezi-Mungu na awaokoe watu wake, amewaletea ukombozi waliobaki wa Israeli!’ Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini, nitawakusanya kutoka miisho ya dunia. Wote watakuwapo hapo; hata vipofu na vilema, wanawake waja wazito na wanaojifungua; umati mkubwa sana utarudi hapa. Watarudi wakiwa wanatoa machozi, nitawarudisha nikiwafariji; nitawapitisha kando ya vijito vya maji, katika njia iliyonyoka ambamo hawatajikwaa; maana mimi nimekuwa baba wa Israeli, Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza. Enyi mataifa, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu, litangazeni katika nchi za mbali, semeni: ‘Aliyemtawanya Israeli, atamkusanya, atamtunza kama mchungaji atunzavyo kondoo wake.’ Maana mimi Mwenyezi-Mungu nimemkomboa Yakobo, nimemwokoa kutoka kwa wenye nguvu kuliko yeye. Watakuja na kuimba kwa sauti juu ya mlima Siyoni, wataona fahari juu ya wema wangu mimi Mwenyezi-Mungu, kwa nafaka, divai na mafuta niwapavyo, kwa kondoo na ng'ombe kadhalika; maisha yao yatakuwa kama bustani iliyotiliwa maji, wala hawatadhoofika tena. Ndipo wasichana wao watafurahi na kucheza, vijana na wazee watashangilia kwa furaha. Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha, nitawafariji na kuwapa furaha badala ya huzuni. Nitawashibisha makuhani kwa vinono, nitawaridhisha watu wangu kwa wema wangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Sauti imesikika mjini Rama, maombolezo na kilio cha uchungu. Raheli anawalilia watoto wake, wala hataki kufarijiwa kwa ajili yao, maana wote hawako tena. Sasa, acha kulia, futa machozi yako, kwani utapata tuzo kwa kazi yako, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema; watoto wenu watarudi kutoka nchi ya maadui zenu. Yapo matumaini kwa siku zenu zijazo, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema; kwani watoto wenu watarejea nchini mwao. “Nimesikia Efraimu akilalamika: ‘Umenichapa ukanifunza nidhamu, kwani nilikuwa kama ndama asiyezoea nira. Unigeuze nami nitakugeukia, kwani wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Maana baada ya kukuasi, nilitubu, na baada ya kufunzwa, nilijilaumu, nikaona haya na kuaibika, maana lawama za ujana wangu ziliniandama.’ “Efraimu ni mwanangu mpendwa; yeye ni mtoto wangu nimpendaye sana. Ndio maana kila ninapomtisha, bado naendelea kumkumbuka. Moyo wangu wamwelekea kwa wema; hakika nitamhurumia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Weka alama katika njia zako, simika vigingi vya kukuongoza, ikumbuke vema ile njia kuu, barabara uliyopita ukienda. Ewe Israeli rudi, rudi nyumbani katika miji yako. Utasitasita mpaka lini ewe binti usiye mwaminifu? Maana, mimi nimefanya kitu kipya duniani: Mwanamke amtafuta mwanamume.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nitakapowafanikisha tena watu wa Israeli, wao watatangaza tena katika nchi ya Yuda na katika miji yake wakisema: ‘Mwenyezi-Mungu akubariki ewe makao adili, akubariki ee mlima mtakatifu!’ “Ndipo watu wa Yuda na miji yake yote, wakulima na wachungaji wanaopitapita na makundi yao, watakaa huko pamoja. Waliochoka nitawachangamsha, na walegevu nitawapa nguvu. Ndio maana mtu ataweza kusema: ‘Niliamka nikatambua kwamba usingizi wangu ulinifaa sana.’” Mwenyezi-Mungu asema: “Tazama, siku zaja ambapo nitaijaza nchi ya Israeli na nchi ya Yuda watu na wanyama kama mkulima asiavyo mbegu. Na kadiri nilivyokuwa mwangalifu kuwangoa, kuwabomoa, kuwaangusha, kuwaharibu na kuwatesa, ndivyo nitakavyokuwa mwangalifu kuwapanda na kuwajenga. Siku hizo watu hawatasema tena: ‘Wazee walikula zabibu chungu, na meno ya watoto yakatiwa ganzi.’ La! Kila mmoja atakufa kwa sababu ya dhambi zake mwenyewe; ni yule tu atakayekula zabibu mbivu ndiye meno yake yatatiwa ganzi.” Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na watu wa Yuda. Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na wazee wao nilipowatoa kwa mkono wangu kutoka Misri; agano hilo walilivunja, ingawa mimi nilikuwa Bwana wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Baada ya siku hizo, nitafanya agano lifuatalo na Waisraeli: Nitaiweka sheria yangu ndani yao, na kuiandika katika mioyo yao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wala haitawabidi kufundishana na kusema: ‘Mjue Mwenyezi-Mungu’, kwa sababu wote, wadogo kwa wakubwa, watanijua mimi Mungu. Maana nitawasamehe makosa yao, wala sitazikumbuka tena dhambi zao.” Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu, ambaye jina lake ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi, aliyepanga jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku, na aifanyaye bahari iwe na mawimbi: Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi hulifanya jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku; pia mimi huitikisa bahari, nayo hutoa mawimbi. Jina langu mimi ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Basi, nami nasema: Kadiri ninavyotegemeza mipango hiyo yote yangu kadiri hiyohiyo Israeli watakavyobaki kuwa watu wangu. Kama mbingu zaweza kupimwa, na misingi ya dunia kuchunguzwa, basi, nitawatupilia mbali wazawa wa Israeli, kwa sababu ya mambo yote waliyotenda. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo mji huu wa Yerusalemu utajengwa upya kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu, kutoka mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni. Nayo kamba ya kupimia itanyoshwa moja kwa moja hadi mlima Garebu, kisha itazungushwa hadi Goa. Bonde lote walimozikwa wafu na kutupiwa majivu, mashamba yote, mpaka kijito cha Kidroni, mpaka pembe ya lango la Farasi kuelekea mashariki, litakuwa eneo takatifu kwa Mwenyezi-Mungu. Hakuna kitakachoharibiwa humo wala kubomolewa tena milele.” Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yeremia mnamo mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia, mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Nebukadneza. Wakati huo, majeshi ya mfalme wa Babuloni yalikuwa yakiuzingira mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ukumbi wa walinzi uliokuwa ndani ya ikulu ya mfalme wa Yuda. Maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga Yeremia akisema, “Kwa nini unatabiri na kusema: ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Tazama, mimi nautia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atauteka. Sedekia, mfalme wa Yuda, hataepa kutiwa mikononi mwa Wakaldayo; hakika atatekwa na mfalme wa Babuloni, ataonana naye uso kwa uso na kuongea naye ana kwa ana. Sedekia atachukuliwa hadi Babuloni, naye atakaa huko mpaka nitakapomchukulia hatua. Hata kama Sedekia atapigana na Wakaldayo, hatashinda.’” Yeremia akasema, Mwenyezi-Mungu alinena nami akasema: “Hanameli, mwana wa baba yako mdogo Shalumu, atakujia na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi, maana wewe ni ndugu yangu kabisa, na unayo haki ya kulikomboa.’” Kisha binamu yangu Hanameli alinijia katika ukumbi wa walinzi kama alivyonifahamisha Mwenyezi-Mungu, akaniambia, “Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini maana wewe una haki ya kulikomboa. Linunue kwa faida yako.” Ndipo nilipotambua kwamba lilikuwa kweli neno la Mwenyezi-Mungu. Basi, nililinunua shamba hilo lililoko Anathothi, kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nikamlipa bei yake shekeli kumi na saba za fedha. Nikaitia sahihi hati ya kumiliki, nikaipiga mhuri, nikawaita mashahidi na kuipima ile fedha katika mizani. Kisha, nilichukua ile hati ya kumiliki niliyoipiga mhuri, ambayo ilikuwa na masharti na kanuni, pamoja na nakala nyingine iliyokuwa wazi. Nilimpa hiyo hati ya ununuzi Baruku mwana wa Neria mwana wa Maaseya, mbele ya binamu yangu Hanameli na mashahidi waliokuwa wametia sahihi hati ya ununuzi, na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ukumbi wa walinzi. Mbele ya watu wote hao, nilimpa Baruku maagizo yafuatayo: Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Chukua hati hizi zote mbili, hati hii ya kumiliki shamba iliyotiwa sahihi, na hii nyingine iliyo wazi, uziweke katika chungu ili zipate kuhifadhiwa kwa muda mrefu.” Maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nyumba na mashamba, pamoja na mashamba ya mizabibu katika nchi hii yatanunuliwa tena.” Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria, hati ya kumiliki shamba nilimwomba Mwenyezi-Mungu nikisema: Ee Mwenyezi-Mungu, ni wewe ambaye kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu, umeziumba mbingu na dunia; hakuna kisichowezekana kwako. Wewe unaonesha fadhili zako kwa maelfu ya watu; lakini pia unawaadhibu watu kwa sababu ya dhambi za wazee wao. Wewe ni Mungu mkuu, mwenye nguvu, Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina lako. Wewe unapanga kwa hekima na unafanya maajabu; njia za watu wote ziko wazi mbele yako, unamlipa kila mmoja kadiri ya njia zake na matendo yake. Katika nchi ya Misri ulifanya maajabu, ukatenda miujiza, na unaendelea kufanya hivyo mpaka leo miongoni mwa Waisraeli na katika mataifa mengine pia, jambo ambalo limekufanya ujulikane kila mahali. Kwa maajabu na miujiza uliyowatisha nayo Wamisri, uliwatoa watu wako Misri kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu. Uliwapa nchi hii ambayo uliahidi kuwapa wazee wao, nchi inayotiririka maziwa na asali. Nao walifika, wakaitwa na kuimiliki. Lakini wao hawakukusikiliza, wala hawakufuata sheria zako. Hawakutenda mambo uliyoamuru. Ndiyo maana utawafanya wapatwe na balaa hii. Tazama, Wakaldayo wamechimba mahandaki kuuzunguka mji; wameuzingira ili wapate kuuteka; wanaushambulia. Vita, njaa na maradhi vitaufanya mji utekwe na watu hao. Kweli mambo uliyotabiri yametokea. Unaona mwenyewe. Lakini, ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe uliyeniambia: “Nunua shamba kwa fedha na kuweka mashahidi,” ingawa mji wenyewe umetekwa na Wakaldayo. Ndipo Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Tazama, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa watu wote. Hakuna lolote linaloweza kunishinda. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninautoa mji huu kwa Wakaldayo na kwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, naye atauteka. Wakaldayo wanaoushambulia mji huu wataingia na kuuchoma moto; watauteketeza pamoja na nyumba ambazo juu ya paa zake ubani ulifukiziwa mungu Baali na tambiko za divai zilimiminiwa miungu mingine, ili kunichokoza. Maana Waisraeli na watu wa Yuda hawakufanya chochote mbele yangu isipokuwa uovu tangu ujana wao; watu wa Israeli hawakufanya chochote isipokuwa kunikasirisha kwa matendo yao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mji huu umechochea hasira yangu na kuniudhi tangu siku ulipojengwa mpaka leo hii. Kwa hiyo, nitautoa kabisa mbele yangu, kwa sababu ya uovu wote waliotenda watu wa Israeli na watu wa Yuda, pamoja na wafalme na viongozi wao, makuhani na manabii wao, na wakazi wa Yerusalemu. Wao walinipa kisogo badala ya kunigeuzia nyuso zao; ingawa nimewafundisha tena na tena, wao hawakusikiliza na kuyapokea mafundisho yangu. Waliweka sanamu za miungu yao ya kuchukiza katika nyumba hii inayojulikana kwa jina langu, wakaitia unajisi. Walimjengea mungu Baali madhabahu katika bonde la Mwana wa Hinomu, ili wamtolee mungu Moleki wavulana wao na binti zao, ingawa sikuwaamuru wala sikufikiria kwamba wangefanya hivyo, wakawafanya watu wa Yuda watende dhambi.” Sasa basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Yeremia, watu hawa wanasema kwamba, kwa vita, njaa na maradhi, mji huu utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babuloni. Lakini nasema: Nitawakusanya watu kutoka nchi zote ambako kwa hasira na ghadhabu na chuki yangu kubwa, niliwatawanya. Nitawarudisha tena mahali hapa, na kuwafanya wakae salama. Nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Nitawapa moyo mmoja na nia moja, wapate kunicha mimi daima, kwa faida yao wenyewe na kwa faida ya watoto wao watakaofuata. Nitafanya nao agano la milele, kwamba sitaacha kamwe kuwatendea mema; nitaweka mioyoni mwao uchaji wangu ili wasiniache tena. Nitafurahi kuwatendea mema; nitawasimika daima katika nchi hii na kuwatendea kwa uaminifu. “Kama nilivyowaletea maafa watu hawa, ndivyo nitakavyowaletea mema niliyowaahidi. Mashamba yatanunuliwa katika nchi hii ambayo unasema imekuwa ukiwa bila watu wala wanyama, na kwamba imetolewa kwa Wakaldayo. Watu watanunua mashamba kwa fedha, watazitilia sahihi hati zake za kuyamiliki, watazipiga mhuri, na kuweka mashahidi katika nchi ya Benyamini, kandokando ya Yerusalemu, katika miji ya Yuda, katika miji ya nchi ya milima, katika miji ya Shefela, na katika miji ya jangwa la Negebu. Maana nitawastawisha tena. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia mara nyingine, wakati alipokuwa bado amefungwa katika ukumbi wa walinzi: Mwenyezi-Mungu aliyeiumba dunia, Mwenyezi-Mungu aliyeifanya na kuiimarisha dunia, ambaye jina lake ni Mwenyezi-Mungu, aliniambia, “Niite, nami nitakujibu na kukuambia mambo makubwa yaliyofichika ambayo hujapata kuyajua. Maana, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema kwamba nyumba za mji wa Yerusalemu na nyumba za wafalme wa Yuda zitabomolewa kwa sababu ya kuzingirwa na kwa sababu ya mashambulizi. Watu watajaribu kuwakabili Wakaldayo lakini hiyo itakuwa bure, maana mahandaki yatajaa maiti za watu ambao nitawaua kwa hasira na ghadhabu yangu. Kwa vile wamefanya uovu huo wote, mimi nitauacha mji huu. “Hata hivyo, mimi nitauponya mji huu na kuwapa watu wake afya; nitawajalia ustawi mwingi na usalama. Nitawastawisha tena watu wa Yuda na watu wa Israeli; nitawaimarisha kama walivyokuwa hapo awali. Nitawatakasa dhambi zao zote na kuwasamehe uovu wao na uasi walionitendea. Nao mji huu utakuwa sababu ya furaha kwangu, mji wa sifa na fahari mbele ya mataifa yote duniani ambayo yatasikia juu ya mema yote ninayowafanyia. Mataifa yataogopa na kutetemeka kwa sababu ya mema na fanaka nitakazouletea mji huu wa Yerusalemu.” Mwenyezi-Mungu asema: “Katika mji huu ambao mnasema umekuwa ukiwa bila watu wala wanyama, naam, katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu ambazo ni tupu, bila watu wala wanyama, humo kutasikika tena sauti za vicheko, sauti za furaha, sauti za harusi na za furaha, sauti za waimbaji wakati wakileta tambiko za shukrani katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu: ‘Mshukuruni Mwenyezi-Mungu wa majeshi kwa kuwa Mwenyezi-Mungu ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele.’ Nitairudishia nchi hii fanaka yake ya awali. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Mahali hapa ambapo ni jangwa bila watu wala wanyama, na katika miji yake yote, patakuwa na malisho ambayo wachungaji watalisha makundi yao ya kondoo. Katika miji ya nchi yenye milima, katika miji ya Shefela na katika miji ya jangwa la Negebu, katika nchi ya Benyamini, kandokando ya mji wa Yerusalemu na katika miji ya Yuda, watu watahesabu tena kondoo wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo nitatimiza ahadi yangu niliyofanya na watu wa Israeli na watu wa Yuda. Katika siku hizo, naam, wakati huo, nitachipusha chipukizi mwadilifu wa uzao wa Daudi. Chipukizi huyo atatekeleza haki na uadilifu katika nchi. Wakati huo nchi ya Yuda itaokolewa na mji wa Yerusalemu utakuwa salama. Na mji huo utaitwa ‘Mwenyezi-Mungu ni Ukombozi Wetu’. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hapatakosekana kamwe mzawa wa Daudi atakayetawala Israeli. Kadhalika nao makuhani wa ukoo wa Lawi watakuwapo daima kunihudumia wakinitolea sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka na kunitolea tambiko milele.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia: “Kama vile hamwezi kutangua agano langu nililoweka kuhusu usiku na mchana hivyo kwamba usiku na mchana visiweko kama nilivyopanga, vivyo hivyo hamwezi kutangua agano langu nililofanya na mtumishi wangu Daudi. Nilifanya agano na Daudi kwamba daima atakuwa na mzawa wa kutawala mahali pake; vilevile kutakuwako daima makuhani wa ukoo wa Lawi watakaonitumikia. Kama vile nyota angani na mchanga wa pwani visivyohesabika, ndivyo nitakavyoongeza idadi ya wazawa wa mtumishi wangu Daudi na idadi ya makuhani wa ukoo wa Lawi.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia: “Je, hujasikia wasemayo watu hawa, kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nimewatupilia mbali watu wa Israeli na watu wa Yuda, jamaa mbili nilizoziteua? Wamewadharau watu wangu, hata kuwaona kwamba wao si taifa. Lakini mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi niliweka agano kuhusu mchana na usiku na kuweka sheria za mbingu na dunia. Basi, ndivyo ilivyo pia: Sitawatupa wazawa wa Yakobo na Daudi, mtumishi wangu; nitamteua mmoja wa wazawa wake atawale wazawa wa Abrahamu, Isaka na Yakobo. Kwa maana nitawarudishia fanaka yao na kuwahurumia.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia wakati Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, pamoja na jeshi lake lote na falme zote za dunia zilizokuwa chini yake, kadhalika na watu wote walipokuwa wakiushambulia mji wa Yerusalemu na miji mingine yote ya kandokando yake: “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli asema hivi: Nenda ukaongee na Sedekia, mfalme wa Yuda. Mwambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nimeutia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atauteketeza kwa moto. Nawe hutatoroka mikononi mwake, bali kwa hakika utatekwa na kupelekwa kwake; utaonana na mfalme wa Babuloni macho kwa macho, na kuongea naye ana kwa ana; kisha, utakwenda Babuloni. Lakini, ewe Sedekia, mfalme wa Yuda, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu yako: Wewe hutauawa kwa upanga vitani. Utakufa kwa amani. Na, kama vile watu walivyochoma ubani walipowazika wazee wako waliokuwa wafalme, ndivyo watakavyokuchomea ubani na kuomboleza wakisema, ‘Maskini! Mfalme wetu amefariki!’ Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Kisha, nabii Yeremia akamweleza Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno hayo yote huko Yerusalemu, wakati jeshi la mfalme wa Babuloni lilipokuwa linaushambulia mji wa Yerusalemu na pia miji ya Lakishi na Azeka, ambayo ilikuwa miji pekee iliyosalia yenye ngome. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu baada ya mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote wa Yerusalemu kuwaachia huru watumwa wao wa Kiebrania wa kiume na wa kike, ili mtu yeyote asimfanye Myahudi mwenzake mtumwa. Viongozi wote na watu wote waliofanya agano hilo walikubaliana wote wawaachie huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na mtu yeyote asiwafanye tena kuwa watumwa. Walikubaliana, wakawaacha huru. Lakini baadaye walibadili nia zao, wakawashika tena watumwa hao wa kiume na wa kike ambao walikuwa wamewaacha huru, wakawafanya watumwa. Hapo neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yeremia: “Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nilifanya agano na wazee wenu nilipowatoa nchini Misri ambako walikuwa watumwa, nikawaambia: ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu atamwacha huru ndugu yake Myahudi aliyeuzwa akawa mtumwa kwa muda wa miaka sita. Mnapaswa kuwaacha huru, wasiwatumikie tena.’ Lakini wazee wenu hawakunisikiliza wala kunitegea sikio. Hivi karibuni nyinyi mlitubu, mkafanya mambo yaliyo sawa mbele yangu, mkawaacha huru Waisraeli wenzenu na kufanya agano mbele yangu katika nyumba yangu. Lakini baadaye mligeuka, mkalitia unajisi jina langu, wakati mlipowachukua tena watumwa walewale wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaachia kama walivyotaka, mkawalazimisha kuwa watumwa tena. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nyinyi hamkunitii kuhusu kuwapatia uhuru ndugu zenu Waisraeli. Basi, nami pia nitawapatieni uhuru; uhuru wa kuuawa kwa upanga vitani, kuuawa kwa maradhi na kwa njaa. Nitawafanya muwe kioja kwa falme zote duniani. Watu waliovunja agano langu na kukataa kufuata masharti ya agano walilofanya mbele yangu, nitawafanya kama yule ndama waliyemkata sehemu mbili na kupita katikati yake. Watu hao ndio hao maofisa wa Yuda, maofisa wa mji wa Yerusalemu, matowashi, makuhani, pamoja na wananchi wote waliopita katikati ya sehemu mbili za yule ndama. Watatiwa mikononi mwa maadui zao, na mikononi mwa watu wanaotaka kuwaua. Maiti zao zitaliwa na ndege wa angani na wanyama wa porini. Naye Sedekia, mfalme wa Yuda, pamoja na viongozi wake, nitawatia mikononi mwa maadui zao, na mikononi mwa watu wanaotaka kuwaua; yaani mikononi mwa jeshi la mfalme wa Babuloni ambalo limeondoka na kuacha kuwashambulia. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema: Nitawaamuru nao wataurudia mji huu. Wataushambulia, watauteka na kuuteketeza kwa moto. Nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa bila wakazi.” Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yeremia wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda: “Nenda nyumbani kwa Warekabu, ukaongee nao. Kisha, walete katika chumba kimojawapo cha nyumba yangu mimi Mwenyezi-Mungu, uwape divai wanywe.” Basi, nikamchukua Yaazania mwana wa Yeremia, mwana wa Habazinia, na ndugu zake pamoja na wanawe wote na ukoo wote wa Warekabu, nikawaleta kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu, katika chumba cha wana wa Hanani mwana wa Igdalia, mtu wa Mungu. Chumba hicho kilikuwa karibu na ukumbi wa wakuu, juu ya ukumbi wa Maaseya mwana wa Shalumu, mlinzi wa ukumbi. Kisha nikaleta vikombe na mabakuli yaliyojaa divai mbele ya hao Warekabu, nikawaambia, “Kunyweni divai.” Lakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, maana Yonadabu mwana wa Rekabu, mzee wetu, alituamuru hivi: ‘Msinywe divai; msinywe nyinyi wenyewe binafsi wala wana wenu milele. Msijenge nyumba, msilime mashamba, wala msiwe na shamba la mizabibu. Lakini mtaishi katika mahema siku zote za maisha yenu, ili mpate kuishi siku nyingi katika nchi mnamoishi kama wageni.’ Sisi tumeitii daima amri hiyo ya mzee wetu Yonadabu mwana wa Rekabu, kuhusu jambo alilotuamuru. Sisi hatunywi kamwe divai; sisi wenyewe hatunywi, wala wake zetu, wala watoto wetu wa kiume au wa kike. Sisi hatujijengei nyumba za kuishi. Hatuna mashamba ya mizabibu wala mashamba ya kulima na kupanda mbegu. Sisi tumeishi katika mahema na kutii mambo yote ambayo Yonadabu, mzee wetu, alituamuru. Lakini Nebukadneza, mfalme wa Babuloni alipofika, kuishambulia nchi hii, tuliamua kuja Yerusalemu ili tuliepe jeshi la Wakaldayo na la Waashuru. Kwa hiyo sasa tunaishi mjini Yerusalemu.” Kisha neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yeremia: “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu hivi: Je, nyinyi hamwezi kupokea mafundisho na kusikia maneno yangu? Ile amri ambayo Yonadabu mwana wa Rekabu, aliwapa wanawe, kwamba wasinywe divai, imefuatwa; nao hawanywi divai mpaka siku hii ya leo, maana wametii amri ya mzee wao. Lakini mimi niliongea nanyi tena na tena, nanyi hamkunisikiliza. Niliwapelekea tena na tena watumishi wangu wote yaani manabii wawaambieni kila mmoja wenu aachane na mwenendo wake mwovu, arekebishe matendo yake na kuacha kuifuata na kuitumikia miungu mingine. Na kwamba mkifanya hivyo mtakaa katika nchi niliyowapa nyinyi na wazee wenu. Lakini nyinyi hamkunitegea sikio wala hamkunisikiliza. Wana wa Yonadabu mwana wa Rekabu, wameshika amri waliyopewa na mzee wao; lakini nyinyi hamkunitii. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Ninawaletea watu wa Yuda na wakazi wote wa Yerusalemu maovu yote niliyotamka dhidi yao, kwa sababu mimi niliongea nao, lakini hawakunisikiliza; niliwaita, lakini hawakuniitikia.” Lakini Yeremia aliwaambia Warekabu hivi: Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nyinyi Warekabu mmetii amri ya mzee wenu, mkashika maagizo yake yote na kutenda kama alivyowaamuru. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema kwamba Yonadabu mwana wa Rekabu hatakosa hata mara moja mzawa wa kunihudumia daima.” Mnamo mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia: “Chukua kitabu uandike humo maneno yote niliyokuambia juu ya Israeli, juu ya Yuda na mataifa yote, tangu siku nilipoanza kuongea nawe, wakati Yosia alipokuwa mfalme mpaka leo. Labda watu wa Yuda watasikia juu ya maovu yote ambayo nimenuia kuwatendea, ili kila mmoja wao auache mwenendo wake mbaya, nami nipate kuwasamehe makosa yao na dhambi yao.” Ndipo Yeremia akamwita Baruku mwana wa Neria. Naye Baruku akaandika katika kitabu maneno yote aliyotamka Yeremia ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia. Kisha, Yeremia akampa Baruku maagizo yafuatayo: “Mimi siruhusiwi kwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Lakini mnamo siku ya kwanza ya mfungo, wewe utakwenda mbele ya umati wote wa watu, ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, usome hati ndefu ya maneno ya Mwenyezi-Mungu niliyokuamuru uandike kama nilivyoyasema. Utayasoma maneno hayo pia mbele ya watu wote wa Yuda waliofika kutoka miji yao. Labda maombi yao yatamfikia Mwenyezi-Mungu na kwamba kila mmoja wao ataacha mwenendo wake mwovu kwa maana Mwenyezi-Mungu ametamka adhabu dhidi ya watu hawa kwa hasira na ghadhabu kali.” Basi, Baruku mwana wa Neria, alitimiza yote aliyoamriwa na nabii Yeremia kuhusu kusoma maneno ya Mwenyezi-Mungu ndani ya nyumba yake Mwenyezi-Mungu kutoka katika kitabu hicho. Mnamo mwaka wa tano wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa tisa, wakazi wote wa Yerusalemu na watu wote waliofika Yerusalemu kutoka miji ya Yuda, walitangaza siku ya mfungo mbele ya Mwenyezi-Mungu. Basi, Baruku alisoma maneno ya Yeremia kutoka katika kile kitabu mbele ya watu wote, ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, katika chumba cha Gemaria mwana wa Shafani aliyekuwa katibu. Chumba hicho kilikuwa katika ukumbi wa juu, kwenye lango Jipya la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Mikaia mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya Mwenyezi-Mungu ambayo yalisomwa kutoka kile kitabu, alikwenda ikulu kwa mfalme katika chumba cha katibu walimokuwa wameketi wakuu wote: Katibu Elishama, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania, na wakuu wote. Mikaia aliwaambia maneno yote aliyoyasikia wakati Baruku aliposoma kitabu mbele ya umati wa watu. Kisha, wakuu walimtuma Yehudi mwana wa Nethania, mjukuu wa Shelemia, kitukuu cha Kushi, amwambie Baruku hivi: “Chukua ile hati ya maandishi uliyosoma mbele ya watu uje nayo hapa.” Basi, Baruku mwana wa Neria, akachukua hati mkononi mwake, akawaendea. Nao wakamwambia: “Keti, uisome.” Baruku akawasomea. Waliposikia maneno hayo yote, walitazamana kwa hofu. Wakamwambia Baruku, “Hatuna budi kumweleza mfalme maneno haya yote.” Kisha wakamwuliza Baruku, “Hebu tuambie, umepataje kuandika maneno yote haya? Je, Yeremia alisema, nawe ukayaandika?” Baruku akawajibu: “Yeye alisema, nami nikawa nayaandika kwa wino katika hati hii.” Kisha wakuu hao wakamwambia Baruku, “Wewe nenda ukajifiche pamoja na Yeremia, na pasiwe na mtu yeyote atakayejua mahali mlipo.” Baada ya wakuu kuweka hati ile ndefu katika chumba cha Elishama katibu wa mfalme, walimwendea mfalme ukumbini, wakamjulisha mambo yote. Kisha, mfalme alimtuma Yehudi aende kuleta ile hati. Yehudi aliichukua kutoka chumbani mwa katibu Elishama, akamsomea mfalme na wakuu wote waliokuwa wamesimama karibu na mfalme. Wakati huo ulikuwa mwezi wa tisa, na mfalme alikuwa ndani ya nyumba yake ya majira ya baridi, akiota moto wa makaa. Ikawa, mara baada ya Yehudi kusoma safu tatu au nne hivi za hiyo hati ndefu, mfalme alizikata safu hizo kwa kisu na kuzitupa katika moto wa makaa. Aliendelea kufanya hivyo mpaka hati yote ikateketea. Lakini, ingawa mfalme na watumishi wake wote waliyasikia maneno hayo yote, hawakuogopa wala kuyararua mavazi yao kwa huzuni. Ijapokuwa Elnata, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asiichome hati hiyo, mfalme hakuwasikiliza. Mfalme alimwamuru Yerameeli mwanawe, Seraya mwana wa Azrieli na Shelemia mwana wa Abdeli, wamkamate katibu Baruku na nabii Yeremia. Lakini Mwenyezi-Mungu aliwaficha. Baada ya mfalme kuchoma moto hati ile ya maneno aliyoandika Baruku kwa maagizo ya Yeremia, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia: “Chukua hati nyingine ndefu, uandike maneno yote yaliyokuwa katika ile hati ya kwanza ambayo Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ameichoma moto. Na huyo Yehoyakimu mfalme wa Yuda, wewe utamwambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Yeye ameichoma moto hati hiyo na kuuliza kwa nini Yeremia ameandika kwamba mfalme wa Babuloni atakuja kuiharibu nchi hii na kuwaangamiza watu na wanyama! Basi, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu yake yeye Yehoyakimu mfalme wa Yuda: Yeye hatakuwa na mzawa atakayekalia kiti cha enzi cha Daudi, na maiti yake itatupwa nje kwenye joto mchana na baridi kali usiku. Nami nitamwadhibu yeye na wazawa wake pamoja na watumishi wake kwa sababu ya uovu wao. Nitawaletea wao na wakazi wote wa Yerusalemu pamoja na watu wote wa Yuda maafa yote niliyotamka dhidi yao na ambayo hawakuyajali.” Kisha, Yeremia alichukua hati nyingine ndefu, akampa katibu Baruku mwana wa Neria, ambaye aliandika humo maneno yote aliyoambiwa na Yeremia ambayo yalikuwa katika ile hati ya awali ambayo Yehoyakimu mfalme wa Yuda, aliichoma moto. Maneno mengine ya namna hiyo yaliongezwa. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni alimtawaza Sedekia mwana wa Yosia, kuwa mfalme wa Yuda mahali pa Konia mwana wa Yehoyakimu. Lakini Sedekia na maofisa wake pamoja na wananchi wa Yuda hawakusikiliza maonyo ya Mwenyezi-Mungu aliyotoa kwa njia ya nabii Yeremia. Mfalme Sedekia aliwatuma Yehukali mwana wa Shelemia, pamoja na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwa nabii Yeremia, wamwombe awaombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Wakati huo, Yeremia alikuwa bado ana uhuru kutembea miongoni mwa watu, maana alikuwa bado hajatiwa gerezani. Tena jeshi la Farao lilikuwa limeondoka Misri, na jeshi la Wakaldayo lililokuwa limeuzingira mji wa Yerusalemu liliposikia habari hizo liliondoka. Ndipo neno la Mwenyezi-Mungu likamjia nabii Yeremia: “Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Utamwambia hivi mfalme wa Yuda ambaye amekutuma uniombe kwa niaba yake: Tazama! Jeshi la Farao lililokuja kukusaidia, liko karibu kurudi makwao Misri. Na Wakaldayo watarudi kuushambulia mji huu. Watauteka mji na kuuteketeza kwa moto. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba msijidanganye wenyewe na kusema kwamba jeshi la Wakaldayo litaondoka; kweli halitaondoka. Hata kama mkilishinda jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki majeruhi tu katika mahema yao, majeruhi hao watainuka na kuuteketeza mji huu kwa moto.” Jeshi la Wakaldayo lilipoondoka Yerusalemu kuliepa jeshi la Farao lililokuwa linakaribia, Yeremia aliondoka Yerusalemu kwenda nchi ya Benyamini ili kupokea sehemu ya urithi wake. Alipokuwa katika lango la Benyamini, mlinzi mmoja aitwaye Iriya mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania, alimkamata Yeremia na kumwambia, “Wewe unatoroka uende kujiunga na Wakaldayo!” Yeremia akamwambia, “Huo ni uongo! Mimi sitoroki na kwenda kujiunga na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakusadiki maneno ya Yeremia. Basi akamtia nguvuni na kumpeleka kwa maofisa. Maofisa hao walimkasirikia sana Yeremia wakampiga, kisha wakamfunga gerezani katika nyumba ya katibu Yonathani iliyokuwa imegeuzwa kuwa gereza. Yeremia alipokuwa amefungwa gerezani kwa muda wa siku nyingi, mfalme Sedekia alimwita na kumkaribisha kwake. Mfalme akamwuliza kwa faragha wakiwa nyumbani mwake; “Je, kuna neno lolote kutoka kwa Mwenyezi-Mungu?” Yeremia akamjibu, “Naam! Lipo!” Kisha akaendelea kusema, “Wewe utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babuloni.” Halafu Yeremia akamwuliza mfalme Sedekia, “Nimekukosea nini, au nimewakosea nini watumishi wako au watu hawa, hata unitie gerezani? Wako wapi manabii waliokutabiria wakisema, ‘Mfalme wa Babuloni hatakushambulia wewe wala nchi hii?’ Sasa nakuomba unisikilize, ee bwana wangu mfalme. Nakusihi sana ulikubali ombi langu. Tafadhali usinirudishe tena gerezani katika nyumba ya katibu Yonathani, nisije nikafia humo.” Basi, mfalme Sedekia akatoa amri Yeremia awekwe katika ukumbi wa walinzi akawa anapewa mkate kila siku kutoka kwa waoka mkate mpaka mikate ilipotoweka kabisa huko mjini. Basi, Yeremia alibaki katika ukumbi wa walinzi. Shefatia mwana wa Matani, Gedalia mwana wa Pashuri, mwana wa Malkia, walisikia maneno ambayo Yeremia aliwatangazia watu wote akisema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Yeyote atakayebaki katika mji huu atakufa kwa vita, njaa na maradhi; lakini yule atakayeondoka na kujisalimisha kwa Wakaldayo, ataishi. Atakuwa ametekwa nyara na kuishi. Mwenyezi-Mungu asema kuwa hakika mji huu utatiwa mikononi mwa jeshi la mfalme wa Babuloni na kutekwa.” Wakuu wakamwambia mfalme, “Yafaa mtu huyu auawe kwa maana anawavunja moyo askari ambao wameachwa katika mji huu na watu wote kwa jumla, kwa kusema maneno kama hayo. Yeye hawatakii watu hawa mema bali mabaya.” Mfalme Sedekia akasema, “Haya! Mtu huyu yumo mikononi mwenu; mimi siwezi kuwapinga.” Basi, wakamchukua Yeremia wakamtumbukiza katika kisima cha Malkia mwana wa mfalme ambacho kilikuwa katika ukumbi wa walinzi. Walimshusha Yeremia ndani kwa kamba. Ndani ya kisima hicho hakukuwa na maji bali tope, naye Yeremia akazama katika tope. Lakini Ebedmeleki, towashi Mwethiopia aliyekuwa akifanya kazi katika ikulu, alipata habari kwamba walikuwa wamemtumbukiza Yeremia kisimani. Wakati huo mfalme alikuwa anabarizi penye lango la Benyamini. Basi, Ebedmeleki akamwendea mfalme, akamwambia, “Bwana wangu mfalme, watu hawa wamefanya kitu kibaya. Wamemtumbukiza yule nabii Yeremia kisimani ambamo kwa kweli atakufa kwa njaa, kwa maana hamna chakula tena mjini.” Hapo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mwethiopia: “Chukua watu watatu kutoka hapa uende ukamtoe nabii Yeremia kisimani, kabla hajafa.” Basi, Ebedmeleki akawachukua watu hao na kwenda pamoja nao ikulu kwa mfalme, wakaingia katika ghala ya ikulu; Ebedmeleki akatwaa nguo zilizotumika na matambara makuukuu, akamteremshia Yeremia kisimani kwa kamba. Kisha Ebedmeleki, Mwethiopia, akamwambia Yeremia, “Weka hayo matambara kwapani mwako, kisha pitisha kamba hizo chini ya matambara hayo.” Yeremia akafanya hivyo. Kisha wakamvuta Yeremia kwa kamba, wakamtoa kisimani. Baada ya hayo, Yeremia akaendelea kukaa katika ukumbi wa walinzi. Wakati fulani mfalme Sedekia alitaka kumwona nabii Yeremia. Basi, akaagiza Yeremia aletwe kwenye mlango wa tatu wa hekalu la Mwenyezi-Mungu. Huko, mfalme alimwambia Yeremia, “Nataka kukuuliza jambo fulani; usinifiche kitu chochote.” Yeremia akamjibu Sedekia, “Je, nikikuambia ukweli hutaniua? Na kama nikikushauri, hutanisikiliza.” Hapo, mfalme Sedekia alimwapia Yeremia kwa siri akisema, “Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu aliyetupa uhai, sitakuua wala sitakutia mikononi mwa hawa wanaotaka kukuua.” Hapo Yeremia akamwambia Sedekia: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Kama ukijitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, utayaokoa maisha yako na mji hautateketezwa kwa moto; nawe pamoja na jamaa yako mtaendelea kuishi. Lakini usipojitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, basi, mji huu utatekwa na Wakaldayo nao watauteketeza kwa moto, nawe hutaweza kujiepusha mikononi mwao.” Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, “Nawaogopa Wayahudi waliokimbilia kwa Wakaldayo. Huenda nikakabidhiwa kwao, wakanitesa.” Yeremia akamjibu, “Hutakabidhiwa kwao. Wewe sasa tii anachosema Mwenyezi-Mungu, kama ninavyokuambia, na mambo yote yatakuendea vema, na maisha yako yatasalimika. Lakini kama ukikataa kujitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwao, haya ndiyo maono ambayo Mwenyezi-Mungu amenionesha. Katika maono hayo, niliona wanawake waliobaki katika ikulu ya mfalme wa Yuda wakipelekwa kwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, nao walikuwa wakisema hivi: ‘Marafiki zako uliowaamini wamekudanganya, nao wamekushinda; kwa kuwa miguu yako imezama matopeni, wamekugeuka na kukuacha.’ Wake zako wote na watoto wako watapelekwa kwa Wakaldayo, nawe mwenyewe hutanusurika. Utachukuliwa mateka na mfalme wa Babuloni na mji huu utateketezwa kwa moto.” Sedekia akamwambia Yeremia: “Mtu yeyote asijue habari hizi, nawe hutauawa. Kama viongozi wakisikia kuwa nimeongea nawe, kisha wakaja na kukuambia, ‘Hebu tuambie, ulizungumza nini na mfalme. Usitufiche chochote nasi hatutakuua’; wewe utawaambia hivi: ‘Nilikuwa ninamsihi mfalme kwa unyenyekevu asinirudishe gerezani nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafia huko.’” Kisha, viongozi walimjia Yeremia wakamwuliza mambo hayo, naye akawajibu kama mfalme alivyomwelekeza. Ndipo walipoacha kuzungumza naye kwa sababu hakuna mtu aliyekuwa amesikia mazungumzo yake na mfalme. Yeremia alibaki katika ukumbi wa walinzi mpaka siku mji wa Yerusalemu ulipotekwa. Mnamo mwezi wa tisa wa mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babuloni alifika na jeshi lake lote kuushambulia mji wa Yerusalemu, akauzingira. Na katika siku ya tisa ya mwezi wa nne, mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa. (Basi maofisa wakuu wafuatao wa mfalme wa Babuloni waliingia na kukaa kwenye lango la katikati: Nergal-shareza, Samgar-nebo, Sar-sekimu mkuu wa matowashi na Nergal-shareza mkuu wa wanajimu, pamoja na maofisa wengine wote wa mfalme wa Babuloni.) Naye Sedekia, mfalme wa Yuda na askari wake wote walipowaona, walitoroka. Walitoka nje ya mji usiku, wakipitia katika bustani ya mfalme, kwenye lango katikati ya kuta mbili, wakaenda upande wa Araba. Lakini jeshi la Wakaldayo liliwafuatia na kumteka Sedekia katika tambarare za Yeriko. Baada ya kumchukua walimfikisha kwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, naye akamhukumu. Hukohuko Ribla, mfalme wa Babuloni aliwaua wana wa Sedekia mbele ya baba yao. Aliwaua pia maofisa wote wa Yuda. Kisha alingoa macho yake Sedekia na kumfunga pingu, ili ampeleke Babuloni. Wakaldayo waliichoma moto ikulu na nyumba za watu; pia walizibomoa kuta za Yerusalemu. Kisha, Nebuzaradani, kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwapeleka uhamishoni Babuloni watu waliokuwa wamebaki mjini na wale waliokuwa wamejisalimisha kwake pamoja na watu wote waliokuwa wamebaki. Nebuzaradani, kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwaacha katika nchi ya Yuda baadhi ya watu maskini ambao hawakuwa na chochote, akawagawia mashamba ya mizabibu na kuwapa maeneo ya kulima wakati huohuo. Nebukadneza mfalme wa Babuloni alikuwa amempa Nebuzaradani kapteni wa walinzi, amri ifuatayo kuhusu Yeremia: “Mchukue Yeremia, umtunze vema wala usimdhuru; mtendee kama anavyokuambia.” Basi, Nebuzaradani kapteni wa walinzi, Nebushani, Nergal-shareza pamoja na maofisa wakuu wote wa mfalme wa Babuloni, wakatuma watu wamtoe Yeremia ukumbini mwa walinzi. Wakamkabidhi Yeremia kwa Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, amchukue nyumbani kwake. Basi, Yeremia akaishi pamoja na wananchi wengine. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia wakati alipokuwa amefungwa katika ukumbi wa walinzi: “Nenda ukamwambie hivi Ebedmeleki, Mwethiopia: Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Tazama mimi nitatimiza mambo yale niliyotamka dhidi ya mji huo na sio mambo mema. Mambo hayo yatakamilika siku hiyo ukiona wewe mwenyewe. Lakini siku hiyo mimi nitakuokoa wewe, wala hutatiwa mikononi mwa watu unaowaogopa. Maana, kweli nitakuokoa na hutauawa vitani; utapata faida ya kuokoa maisha yako kwa sababu umeniamini mimi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu wakati Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, alipomruhusu Yeremia aondoke Rama. Huyo kapteni alimchukua Yeremia amefungwa minyororo, akawachukua pia pamoja naye mateka wengine wote wa Yerusalemu na Yuda ambao walikuwa wamepelekwa uhamishoni Babuloni. Kapteni wa walinzi alimchukua Yeremia, akamwambia “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, alitangaza maafa dhidi ya mahali hapa. Na sasa Mwenyezi-Mungu ametekeleza jambo hilo na kutenda kama alivyosema, kwa sababu nyinyi nyote mlimkosea Mwenyezi-Mungu na kukataa kumtii, jambo hilo limewapata. Haya! Leo nazifungua pingu mikononi mwako. Kama unaona ni vema kwenda pamoja nami mpaka Babuloni, basi twende pamoja; mimi nitakutunza vizuri. Lakini kama unaona si vizuri kwako kwenda pamoja nami mpaka Babuloni, basi, usije. Ujue kwamba waweza kwenda popote katika nchi hii; basi nenda popote unapoamua kuwa pazuri kwenda. Kama ukiamua kubaki, basi rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, ambaye mfalme wa Babuloni amemteua kuwa mtawala wa miji yote ya Yuda, ukakae naye miongoni mwa wananchi wengine. La sivyo, nenda popote unapoona ni sawa kwenda.” Basi, kapteni wa walinzi akampa Yeremia masurufu na zawadi, kisha akamwacha aende zake. Kisha Yeremia akaenda Mizpa kwa Gedalia mwana wa Ahikamu, akakaa naye pamoja na wananchi waliobaki nchini. Makapteni wote wa majeshi kutoka bara pamoja na watu wao, waliposikia kwamba mfalme wa Babuloni alikuwa amemtawaza Gedalia mwana wa Ahikamu, kuwa mkuu wa nchi, na kwamba alikuwa amemkabidhi wanaume, wanawake na watoto, yaani watu mafukara kabisa katika nchi ambao hawakuchukuliwa uhamishoni Babuloni, walimwendea Gedalia huko Mizpa. Watu hao walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani na Yonathani wana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi, wana wa Efai kutoka Netofa, na Yezania mwana wa Maakathi; wote waliandamana na watu wao. Gedalia aliapa mbele yao na mbele ya majeshi yao akisema: “Msiogope kuwatumikia Wakaldayo. Kaeni nchini mumtumikie mfalme wa Babuloni, na mambo yote yatawaendea vema. Mimi nitakaa Mizpa niwawakilishe nyinyi kwa Wakaldayo watakaofika kwetu; lakini nyinyi kusanyeni na kuhifadhi divai, matunda ya kiangazi na mafuta, mkae katika miji mnayoimiliki.” Pia watu wa Yuda waliokuwa nchini Moabu na miongoni mwa Waamoni na nchini Edomu na nchi nyingine, waliposikia kwamba mfalme wa Babuloni alikuwa amewaruhusu watu wa Yuda wengine kubaki Yuda na kwamba alikuwa amemweka Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, kuwa mtawala wao, wote walirudi kutoka mahali pote walipokuwa wametawanyika na kwenda katika nchi ya Yuda kwa Gedalia huko Mizpa. Walichuma zabibu na matunda ya kiangazi kwa wingi sana. Basi, Yohanani mwana wa Karea pamoja na viongozi wote wa majeshi kutoka bara, walifika kwa Gedalia, huko Mizpa, wakamwambia, “Je, una habari kwamba Baali mfalme wa Waamoni, amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania, akuue?” Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu, hakuamini maneno yao. Kisha, Yohanani mwana wa Karea, akazungumza na Gedalia kwa faragha huko Mizpa, akamwambia, “Acha niende nikamuue Ishmaeli mwana wa Nethania, na hakuna mtu yeyote atakayejua. Kwa nini yeye akuue na watu wa Yuda wote waliokusanyika hapa watawanyike na Wayahudi waliobaki waangamie?” Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu, akamwambia Yohanani mwana wa Karea, “Usifanye jambo hilo! Mambo unayosema juu ya Ishmaeli si ya kweli!” Mnamo mwezi wa saba, Ishmaeli mwana wa Nethania, mjukuu wa Elishama, wa ukoo wa kifalme, mmoja wa maofisa wakuu wa mfalme, alifika Mizpa kwa Gedalia akiandamana na watu kumi. Wakati walipokuwa wanakula chakula huko Mizpa, Ishmaeli mwana wa Nethania pamoja na wale watu kumi, wakainuka na kumshambulia kwa upanga Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, wakamuua. Gedalia ndiye aliyekuwa ameteuliwa na mfalme wa Babuloni kuwa mtawala wa nchi. Ishmaeli aliwaua pia Wayahudi wote waliokuwa pamoja na Gedalia huko Mizpa na wanajeshi Wakaldayo waliokuwa mahali hapo. Siku moja baada ya kumwua Gedalia, kabla hata mtu yeyote hajajua habari hizo, walifika watu themanini kutoka Shekemu, Shilo na Samaria. Walikuwa wamenyoa ndevu zao na wamevaa mavazi yaliyotatuka na miili yao imechanjwachanjwa. Walileta tambiko za nafaka na ubani zitolewe hekaluni kwa Mwenyezi-Mungu. Ishmaeli mwana wa Nethania, alitoka nje ya mji kuwalaki watu hao huku analia. Alipokutana nao, akawaambia, “Karibuni nyumbani kwa Gedalia mwana wa Ahikamu.” Walipoingia mjini, Ishmaeli mwana wa Nethania, pamoja na wale watu kumi waliokuwa pamoja naye, waliwaua watu hao na kuzitupa maiti zao kisimani. Lakini palikuwa na watu kumi katika kundi hilo waliomwambia Ishmaeli: “Tafadhali usituue, maana tuna akiba kubwa ya ngano, shayiri, mafuta na asali ambayo tumeificha mashambani.” Basi hao akawaacha hai. Kisima ambamo Ishmaeli alitupa maiti za wale watu aliowaua kilikuwa ni kile kikubwa, ambacho mfalme Asa alikuwa amekichimba ili kujihami dhidi ya Baasha, mfalme wa Waisraeli. Ishmaeli mwana wa Nethania, alikijaza kisima hicho maiti za wale watu aliowaua. Kisha, Ishmaeli aliwateka binti zake mfalme na watu wote waliosalia Mizpa, watu ambao Nebuzaradani, kapteni wa walinzi, alikuwa amemkabidhi Gedalia mwana wa Ahikamu. Ishmaeli mwana wa Nethania, aliwachukua mateka hao, akaondoka, akaenda kwa Waamoni. Lakini Yohanani mwana wa Karea, pamoja na viongozi wote wa majeshi, waliposikia juu ya uovu ambao Ishmaeli mwana wa Nethania, alikuwa ameufanya, waliwakusanya watu wao wote, wakaenda kupigana na Ishmaeli. Walimkuta penye bwawa kuu lililoko Gibeoni. Watu wote waliotekwa na Ishmaeli walipomwona Yohanani mwana wa Karea, pamoja na viongozi wote wa majeshi, walifurahi sana. Basi, watu hao wote ambao Ishmaeli alikuwa amewachukua mateka kutoka Mizpa, waligeuka, wakarudi nyuma, wakamwendea Yohanani mwana wa Karea. Lakini Ishmaeli mwana wa Nethania, pamoja na watu wanane waliponyoka kutoka kwa Yohanani, wakakimbilia kwa Waamoni. Kisha, Yohanani mwana wa Karea pamoja na viongozi wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, waliwachukua watu wote waliosalia, ambao Ishmaeli mwana wa Nethania, alikuwa amewachukua mateka kutoka Mizpa baada ya kumwua Gedalia mwana wa Ahikamu, yaani: Askari, wanawake, watoto na matowashi. Yohanani aliwarudisha wote kutoka Gibeoni. Basi, wakaenda zao, wakakaa huko Geruthi Kimahamu karibu na Bethlehemu, wakikusudia kuingia katika nchi ya Misri, kwa sababu walikuwa wanawaogopa Wakaldayo tangu wakati Ishmaeli mwana wa Nethania, alipomuua Gedalia mwana wa Ahikamu ambaye mfalme wa Babuloni alikuwa amemteua kuwa mtawala wa nchi. Kisha makamanda wote wa majeshi, Yohanani mwana wa Karea, na Azaria mwana wa Heshaia pamoja na watu wote, wadogo kwa wakubwa, wakamwendea Yeremia, wakamwambia, “Tafadhali sikiliza maombi yetu na kutuombea dua kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, sisi sote tuliosalia (kwa maana tulikuwa wengi, lakini sasa tumebaki wachache tu, kama uonavyo). Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na atuoneshe njia anayotaka tuifuate, na kile anachotaka tukifanye.” Yeremia akawajibu, “Vema; nimesikia. Nitamwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kama mlivyonisihi; jibu lolote atakalonipa Mwenyezi-Mungu, nitawaambieni; sitawaficha chochote.” Kisha, watu wakamwambia Yeremia, “Mwenyezi-Mungu na awe shahidi wa kweli na mwaminifu dhidi yetu ikiwa hatutafanya jinsi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atakavyokuagiza utuambie. Iwe ni jambo la kupendeza au la, sisi tutaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu ambaye tunakutuma kwake ili tufanikiwe tutakapomtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.” Baada ya siku kumi, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia. Basi, Yeremia akamwita Yohanani mwana wa Karea, na makamanda wote wa majeshi pamoja na watu wote, wadogo kwa wakubwa, akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli ambaye mlinituma kwake nipeleke maombi yenu, asema hivi: Kama mtabaki katika nchi hii, basi, nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawaotesha wala sitawangoa; kwa maana nitabadili nia kwa sababu ya maafa niliyowatenda. Msimwogope mfalme wa Babuloni mnayemwogopa; naam, msimwogope hata kidogo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mimi niko pamoja nanyi kuwaokoeni na kuwasalimisha kutoka mikononi mwake. Nitawahurumieni na kumfanya mfalme awahurumie na kuwaacha nchini mwenu. “Lakini mkisema: ‘Hatutaki kubaki katika nchi hii,’ na hivyo mkaacha kutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kusema kwamba mtakwenda kukaa nchini Misri, ambako hamtaona vita wala kusikia sauti ya tarumbeta wala kukosa chakula, basi, sikilizeni asemavyo Mwenyezi-Mungu enyi mabaki ya Yuda. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: Kama mmekusudia kuingia nchini Misri na kukaa huko, basi, vita mnavyoviogopa vitawakumba hukohuko Misri, na njaa mnayoihofia itawaandama vikali hadi Misri, na mtafia hukohuko. Watu wote wenye nia ya kwenda kukaa Misri watakufa kwa njaa na maradhi mabaya wala hakuna hata mmoja wao atakayebaki au kunusurika kutokana na maafa nitakayowaletea. “Maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Kama vile hasira yangu na ghadhabu yangu ilivyowapata wakazi wa Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyowapata nyinyi, kama mtakwenda Misri. Mtakuwa kitu cha kutukanwa, kitisho, laana na aibu. Hamtapaona tena mahali hapa.” Yeremia akawaambia watu: “Enyi Wayahudi mliosalia, Mwenyezi-Mungu aliwaambia msiende Misri. Jueni wazi kwamba leo nimewaonya kuwa mmepotoka, mmeyahatarisha maisha yenu. Maana mlinituma kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkiniambia, ‘Tuombee dua kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, na chochote Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu atakachosema, utuambie, nasi tutatekeleza.’ Leo mimi nimewaambieni lakini hamkutii chochote ambacho Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amenituma niwaambie. Basi, jueni hakika kwamba mahali mnapotamani kwenda kukaa mtafia hukohuko kwa vita, njaa na maradhi.” Yeremia alipomaliza kuwaambia watu wote maneno yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, alimwamuru awatangazie, Azaria mwana wa Hoshaia, Yohanani mwana wa Karea na watu wote mafidhuli, walimwambia Yeremia: “Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, hakukutuma wewe utuambie tusiende Misri, tukaishi huko. Baruku mwana wa Neria, amekuchochea dhidi yetu ili tutiwe mikononi mwa Wakaldayo watuue au watupeleke uhamishoni Babuloni.” Basi, Yohanani mwana wa Karea na makamanda wote wa majeshi pamoja na watu wote hawakutii aliyosema Mwenyezi-Mungu, kwamba wabaki katika nchi ya Yuda. Hapo Yohanani mwana wa Karea na makamanda wote wa majeshi waliwachukua watu wote wa Yuda waliosalia ambao walikuwa wamerudi nchini Yuda kutoka mataifa yote ambako walikuwa wametawanywa; wanaume, wanawake, watoto, binti za mfalme na kila mtu ambaye Nebuzaradani, kapteni wa walinzi, alikuwa amemwachia Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, wakamchukua pia nabii Yeremia na Baruku mwana wa Neria, wakaenda nchini Misri, wakawasili mjini Tahpanesi. Ndivyo walivyokataa kutii alichosema Mwenyezi-Mungu Basi neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yeremia huko Tahpanesi: “Chukua mawe makubwa, ukayafiche katika chokaa ya matofali kwenye lango la ikulu ya Farao mjini Tahpanesi, watu wa Yuda wakiwa wanaona. Kisha waambie hivi: Tazameni mimi nitamtuma na kumleta Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, mtumishi wangu, naye ataweka kiti chake cha enzi juu ya mawe haya ambayo nimeyaficha hapa, na kutandaza paa la kifalme juu yake. Atakapofika ataiangamiza nchi ya Misri. Hapo waliopangiwa kufa kwa maradhi watakufa kwa maradhi, waliopangiwa kuchukuliwa mateka, watachukuliwa mateka; waliopangiwa kufia vitani watafia vitani. Mimi nitawasha moto katika mahekalu ya miungu ya Misri; naye Nebukadneza ataiteketeza miungu hiyo kwa moto au kuichukua mateka mpaka Babuloni. Ataisafisha nchi ya Misri kama mchungaji atoavyo kupe katika vazi lake na kuondoka Misri akiwa mshindi. Ataivunja minara ya ukumbusho iliyoko huko Heliopoli nchini Misri, na mahekalu ya miungu ya Misri atayateketeza kwa moto.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia kuhusu Wayahudi waliokuwa wanakaa nchini Misri katika miji ya Migdoli, Tahpanesi, Memfisi na sehemu ya Pathrosi: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi: Nyinyi mmeona maafa yote niliyouletea mji wa Yerusalemu na miji yote ya Yuda. Miji hii ni magofu mpaka leo wala hakuna mtu aishiye humo. Imekuwa hivyo kwa sababu ya uovu walioufanya, wakanikasirisha kwa kuifukizia ubani na kuitumikia miungu mingine ambayo wao wenyewe hawakuifahamu, wala nyinyi, wala wazee wenu. Hata hivyo, mimi daima niliwatuma kwenu watumishi wangu manabii nikisema: Msifanye jambo hili baya ninalolichukia! Lakini hakuna aliyenisikiliza wala kunitegea sikio. Nyinyi mlikataa kuacha uovu wenu na kuacha kuifukizia ubani miungu mingine. Kwa hiyo, ghadhabu yangu na hasira yangu iliwaka na kumiminika juu ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, hata kukawa jangwa na magofu kama ilivyo mpaka leo. “Sasa, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nauliza hivi: Mbona mnajiletea madhara makubwa namna hii, na kujiangamiza nyinyi wenyewe, wanaume kwa wanawake, watoto wadogo na wachanga, hata pasibaki mtu katika Yuda? Kwa nini mnanichochea nikasirike kwa kuabudu sanamu mlizojitengenezea wenyewe na kuifukizia ubani miungu mingine katika nchi ya Misri ambamo mmekuja kuishi? Je, mwataka kutokomezwa na kuwa laana na dhihaka mbele ya mataifa yote duniani? Je, mmesahau uovu wa wazee wenu, uovu wa wafalme wa Yuda, uovu wa wake zao na uovu wenu nyinyi wenyewe na wa wake zenu, ambao mliufanya nchini Yuda na kwenye barabara za Yerusalemu? Mpaka hivi leo hamjajinyenyekesha wala kuogopa wala kuzifuata sheria zangu na kanuni zangu nilizowawekea nyinyi na wazee wenu. “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Haya! Nitawageukia niwaleteeni maafa na kuiangamiza Yuda yote. Nitawaondoa watu wa Yuda waliosalia ambao wamepania kwenda kukaa Misri, na kuwaangamiza wote, wakubwa kwa wadogo; watakufa kwa upanga au kwa njaa. Watakuwa takataka, kitisho, laana na dhihaka. Nitawaadhibu wale wanaokaa katika nchi ya Misri kama nilivyouadhibu mji wa Yerusalemu, kwa vita, njaa, na maradhi mabaya. Kwa hiyo hapatakuwa na mtu hata mmoja kati ya watu wa Yuda waliosalia na kwenda kukaa katika nchi ya Misri ambaye atanusurika au kuishi au kurudi katika nchi ya Yuda ambayo wanatamani kurudi na kuishi humo. Hawatarudi, isipokuwa baadhi ya wakimbizi.” Kisha, wanaume wote waliojua kwamba wake zao walikuwa wameifukizia ubani miungu mingine, na wanawake wote waliokuwa hapo, kusanyiko kubwa la watu, pamoja na Waisraeli waliokuwa wanakaa Pathrosi katika nchi ya Misri walimjibu Yeremia: “Jambo hilo ulilotuambia kwa niaba ya Mwenyezi-Mungu hatutalitii. Lakini kila kitu tulichoapa kufanya tutafanya: Tutamfukizia ubani malkia wa mbinguni na kummiminia tambiko ya kinywaji kama tulivyokuwa tunafanya sisi wenyewe na wazee wetu, wafalme wetu na viongozi wetu, katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Ama wakati huo tulikuwa na chakula tele, tulistawi na hatukuona janga lolote. Lakini tangu tuache kumfukizia ubani malkia wa mbinguni na kummiminia kinywaji, tumetindikiwa kila kitu, na tumeangamizwa kwa vita na njaa.” Nao wanawake wakasema, “Tulimfukizia ubani na kummiminia kinywaji malkia wa mbinguni. Tulifanya hivyo kwa kibali cha waume zetu. Tena tulimtengenezea mikate yenye sura yake na kummiminia kinywaji!” Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume kwa wanawake, yaani watu wote waliompa jibu hilo: “Kuhusu matambiko ambayo nyinyi na wazee wenu, wafalme wenu na viongozi wenu, pamoja na wananchi wote, mlifanya katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu, je, mnadhani Mwenyezi-Mungu amesahau au hakumbuki? Mwenyezi-Mungu hakuweza kuvumilia tena matendo yenu maovu na mambo ya kuchukiza mliyotenda; ndiyo maana nchi yenu imekuwa ukiwa, jangwa, laana na bila wakazi, kama ilivyo mpaka leo. Maafa haya yamewapata mpaka leo kwa sababu mliitolea sadaka za kuteketezwa miungu mingine na kumkosea Mwenyezi-Mungu, mkakataa kutii sauti yake au kufuata sheria yake, kanuni zake na maagizo yake.” Yeremia aliwaambia watu wote na wanawake wote: “Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi watu wa Yuda wote mlioko nchini Misri. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Nyinyi pamoja na wake zenu mmetekeleza kwa vitendo yale mliyotamka kwa vinywa vyenu, mkisema kwamba mmepania kutimiza viapo vyenu mlivyofanya vya kumtolea sadaka na kummiminia kinywaji malkia wa mbinguni. Haya basi! Shikeni viapo vyenu na kutoa sadaka za vinywaji! Lakini sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu, enyi watu wote wa Yuda mnaokaa nchini Misri. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Naapa kwa jina langu kuu kwamba hakuna mtu yeyote wa Yuda katika nchi yote ya Misri atakayelitumia jina langu kuapa nalo akisema: ‘Kama aishivyo Bwana Mwenyezi-Mungu!’ Mimi nawachungulia hao sio kwa mema bali kwa mabaya. Watu wote wa Yuda nchini Misri wataangamizwa kwa upanga na njaa, asibaki hata mtu mmoja. Ni wachache watakaonusurika vitani na kurudi kutoka nchi ya Misri na kwenda nchini Yuda. Hapo watu wa Yuda wote waliobaki kati ya wale waliokwenda kukaa Misri watatambua ni tamko la nani lenye nguvu: Langu au lao! Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba nitawaadhibu hapahapa mpate kujua kwamba maneno ya maafa niliyotamka dhidi yenu yatatimia. Na hii itakuwa ishara yake: Nitamtia Farao Hofra mfalme wa Misri, mikononi mwa madui zake, mikononi mwa wale wanaotaka kumwua, kama vile nilivyomtia Sedekia mfalme wa Yuda, mikononi mwa adui yake yaani Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, ambaye alitaka kumwua. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Haya ndiyo maneno aliyotamka nabii Yeremia mnamo mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia naye Baruku mwana wa Neria akawa anayaandika kitabuni. Yeremia alimwambia Baruku: “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi juu yako wewe Baruku: Wewe ulisema, ‘Ole wangu! Mwenyezi-Mungu ameniongezea uchungu juu ya maumivu yangu. Nimechoka kupiga kite, wala sipati pumziko.’ Lakini Mwenyezi-Mungu ameniambia nikuambie hivi: Tazama, yale niliyojenga nayabomoa, na yale niliyopanda nayangoa; nitafanya hivyo katika nchi yote. Je, wewe unajitakia mambo makubwamakubwa? Usiyatafute! Achana nayo, maana, ninaleta maangamizi juu ya wanadamu wote. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wewe tuzo lako ni hili: Nitayaokoa maisha yako kila mahali utakapokwenda.” Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yeremia kuhusu watu wa mataifa. Kuhusu Misri na jeshi la Farao Neko mfalme wa Misri, lililokuwa huko Karkemishi karibu na mto Eufrate ambalo Nebukadneza mfalme wa Babuloni alilishambulia mnamo mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda: Tayarisheni ngao ndogo na kubwa msonge mbele kupigana vita. Tandikeni farasi na kuwapanda, Shikeni nafasi zenu na kofia za chuma mvae. Noeni mikuki yenu, vaeni mavazi yenu ya chuma! Lakini mbona nawaona wametishwa? Wamerudi nyuma. Mashujaa wao wamepigwa, wamekimbia mbio, bila hata kugeuka nyuma. Kitisho kila upande. Mwenyezi-Mungu amesema. Walio wepesi kutoroka hawawezi, mashujaa hawawezi kukwepa; huko kaskazini kwenye mto Eufrate wamejikwaa na kuanguka. Nani huyo aliye kama mto Nili uliofurika kama mito inayoumuka mawimbi? Misri ni kama mto Nili uliofurika kama mito inayoumuka mawimbi Ilisema: “Nitajaa, nitaifunika nchi, nitaiharibu miji na wakazi wake. Songeni mbele, enyi farasi, shambulieni enyi magari ya farasi. Mashujaa wasonge mbele: Watu wa Kushi na Puti washikao ngao, watu wa Ludi, stadi wa kutumia pinde.” Siku hiyo ni siku ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ni siku ya kulipiza kisasi; naam, siku ya kuwaadhibu maadui zake. Upanga utawamaliza hao na kutosheka, utainywa damu yao na kushiba. Maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi anayo kafara huko kaskazini karibu na mto Eufrate. Pandeni Gileadi, enyi watu wa Misri, mkachukue dawa ya marhamu. Mmetumia dawa nyingi bure; hakuna kitakachowaponya nyinyi. Mataifa yamesikia aibu yenu, kilio chenu kimeenea duniani kote; mashujaa wamegongana wenyewe kwa wenyewe, wote pamoja wameanguka. Neno ambalo Mwenyezi-Mungu alimwambia Yeremia wakati alipofika Nebukadneza mfalme wa Babuloni kuishambulia nchi ya Misri: “Tangaza nchini Misri, piga mbiu huko Migdoli, tangaza huko Memfisi na Tahpanesi. Waambie: ‘Kaeni tayari kabisa maana upanga utawaangamiza kila mahali.’ Kwa nini shujaa wako amekimbia? Mbona fahali wako hakuweza kustahimili? Kwa sababu mimi Mwenyezi-Mungu nilimwangusha chini! Wengi walijikwaa, wakaanguka, kisha wakaambiana wao kwa wao: ‘Simameni, tuwaendee watu wetu, turudi katika nchi yetu, tuukimbie upanga wa adui.’ “Naye Farao, mfalme wa Misri, mpangeni jina hili: ‘Kishindo kitupu!’ Mimi naapa kwa uhai wangu nasema mimi mfalme niitwaye Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kweli adui anakuja kuwashambulieni: Ni hakika kama Tabori ulivyo mlima kama mlima Karmeli uonekanavyo kutoka baharini. Enyi wakazi wa Misri jitayarisheni na mizigo kwenda uhamishoni! Maana mji wa Memfisi utaharibiwa kabisa, utakuwa magofu yasiyokaliwa na watu. Misri ni kama mtamba mzuri wa ng'ombe, lakini kipanga kutoka kaskazini amemvamia. Hata askari wake wa kukodiwa ni kama ndama wanono; nao pia wamegeuka, wakakimbia pamoja, wala hawakuweza kustahimili, kwa maana siku yao ya kuangamizwa imefika, wakati wao wa kuadhibiwa umewadia. Misri anatoa sauti kama nyoka anayekimbia; maana maadui zake wanamjia kwa nguvu, wanamjia kwa mashoka kama wakata-miti. Wataukata kabisa msitu wake, ingawa haupenyeki, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, maana wao ni wengi kuliko nzige wasiohesabika. Watu wa Misri wataaibishwa, watatiwa mikononi mwa watu kutoka kaskazini.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, alisema: “Tazama, mimi nitamwadhibu Amoni mungu wa Thebesi, nitaiadhibu Misri na miungu yake na wafalme wake, nitamwadhibu Farao na wote wanaomtegemea. Nitawatia mikononi mwa wale wanaotaka kuyaangamiza maisha yao, yaani Nebukadneza mfalme wa Babuloni na maofisa wake. Baadaye, nchi ya Misri itakaliwa na watu kama ilivyokuwa hapo zamani. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Lakini wewe usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu, usifadhaike, ee Israeli; maana, kutoka mbali nitakuokoa, nitakuja kuwaokoa wazawa wako kutoka nchi walimohamishwa. Yakobo utarudi na kutulia na kustarehe, wala hakuna yeyote atakayekutia hofu. Usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu, kwa maana mimi niko pamoja nawe. Nitayaangamiza kabisa mataifa yote ambayo nimekutawanya kati yao, lakini wewe sitakuangamiza. Nitakuchapa kadiri unavyostahili, sitakuacha bila kukuadhibu.” Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaushambulia mji wa Gaza: Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Tazama! Maji yanapanda kutoka kaskazini, nayo yatakuwa mto uliofurika; yataifunika nchi nzima na vyote vilivyomo, mji na wakazi na wanaoishi humo. Watu watalia, wakazi wote wa nchi wataomboleza. Watasikia mshindo wa kwato za farasi, kelele za magari ya vita, na vishindo vya magurudumu yao. Kina baba watawasahau watoto wao, mikono yao itakuwa imelegea mno. Hiyo ni siku ya kuwaangamiza Wafilisti wote, kukomesha msaada uliobakia kutoka Tiro na Sidoni. Maana Mwenyezi-Mungu anawaangamiza Wafilisti, watu waliosalia wa kisiwa cha Kaftori. Watu wa Gaza wamenyoa upara kuomboleza; mji wa Ashkeloni umeangamia. Enyi watu wa Anakimu mliobaki mpaka lini mtajikatakata kwa huzuni? Ee upanga wa Mwenyezi-Mungu! Utachukua muda gani ndipo utulie? Ingia katika ala yako, ukatulie na kunyamaa! Lakini utawezaje kutulia, hali Mwenyezi-Mungu ameupa kazi? Ameuamuru ushambulie mji wa Ashkeloni na watu wanaoishi pwani.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Ole watu wa Nebo, maana mji wake umeharibiwa! Kiriathaimu umeaibishwa, umetekwa, ngome yake imebomolewa mbali; fahari ya Moabu imetoweka. Mpango ulifanywa huko Heshboni dhidi yake: ‘Haya! Tuwaangamize wasiwe tena taifa!’ Nawe Madmeni utanyamazishwa, upanga utakufuatia. Sikiliza! Kilio kutoka Horonaimu: ‘Maangamizi na uharibifu mkubwa!’ Moabu tayari imeangamizwa kilio chake chasikika mpaka Soari. Walionusurika wanapanda kwenda Luhithi huku wanalia kwa sauti. Wanapoteremka kwenda Horonaimu, wanasikia kilio cha uharibifu. Kimbieni! Jiokoeni wenyewe! Kimbieni kama pundamwitu jangwani! “Moabu, ulitumainia ngome na hazina zako, lakini sasa wewe pia utatekwa; mungu wako Kemoshi atapelekwa uhamishoni pamoja na makuhani na watumishi wake. Mwangamizi atapita katika kila mji, hakuna mji utakaomwepa; kila kitu mabondeni kitaangamia nyanda za juu zitaharibiwa, kama alivyosema Mwenyezi-Mungu. Mchimbieni Moabu kaburi, maana kuangamia kwake ni hakika; miji yake itakuwa tupu, bila mkazi hata mmoja. Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Mwenyezi-Mungu kwa ulegevu; alaaniwe anayezuia upanga wake usimwage damu! Moabu amestarehe tangu ujana wake, ametulia kama divai katika gudulia. Hajamiminiwa toka chombo hata chombo, hajapata kuchukuliwa uhamishoni. Kwa hiyo yungali na ladha yake, harufu yake nzuri haijabadilika kamwe. “Kwa hiyo, wakati waja, nasema mimi Mwenyezi-Mungu ambapo nitampelekea wamiminaji ambao wataimimina divai yake. Wataimwaga yote kutoka vyombo vyake na kuvivunja vipandevipande. Hapo Wamoabu watamwonea aibu mungu wao Kemoshi, kama vile watu wa Israeli walivyomwonea aibu Betheli, mungu waliyemtegemea. Mwawezaje kusema: ‘Sisi ni mashujaa, na watu wenye nguvu nyingi za vita?’ Mwangamizi wa Moabu na miji yake amewasili vijana wake wazuri wamechinjwa. Nimesema mimi mfalme niitwaye Mwenyezi-Mungu wa Majeshi. Janga la Moabu limekaribia, maangamizi yake yanawasili haraka. Mwomboleezeni Moabu, enyi jirani zake wote, na nyote mnaomjua vizuri semeni: ‘Jinsi gani fimbo ya nguvu ilivyovunjwa, naam fimbo ile ya fahari!’ Enyi wenyeji wa Diboni: Shukeni kutoka mahali penu pa fahari, mkaketi katika ardhi isiyo na maji. Maana mwangamizi wa Moabu, amefika kuwashambulia; amekwisha haribu ngome zenu. Enyi wakazi wa Aroeri, simameni kando ya njia mtazame! Mwulizeni anayekimbia na anayetoroka: ‘Kumetokea nini?’ Moabu imeaibishwa maana imevunjwa; ombolezeni na kulia. Tangazeni kando ya mto Arnoni, kwamba Moabu imeharibiwa kabisa. “Hukumu imeifikia miji iliyo nyanda za juu: Holoni, Yasa, Mefaathi, Diboni, Nebo, Beth-diblathaimu, Kiriathaimu, Beth-gamuli, Beth-meoni, Keriothi na Bosra. Naam, hukumu imeifikia miji yote ya Moabu mbali na karibu. Nguvu za Moabu zimevunjiliwa mbali na uwezo wake umevunjwa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Mlewesheni Moabu kwa sababu alijikuza dhidi yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Moabu atagaagaa katika matapishi yake na watu watamcheka. Kumbuka Moabu ulivyomcheka Israeli. Je, alikamatwa pamoja na wezi, hata ukawa unatikisa kichwa chako kila ulipoongea juu yake? “Enyi wenyeji wa Moabu, tokeni mijini, mkakae mapangoni! Mwigeni njiwa ajengaye kiota penye genge. Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu; Moabu ana majivuno sana. Tumesikia juu ya kujiona, kiburi na majivuno yake; tumesikia jinsi anavyojigamba moyoni. “Nami Mwenyezi-Mungu nasema: Najua ufidhuli wake; Majivuno yake ni ya bure, na matendo yake si kitu. Kwa hiyo ninaomboleza juu ya Moabu, ninalia kwa ajili ya Wamoabu wote, naomboleza juu ya watu wa Kir-heresi. Nakulilia wewe bustani ya Sibma kuliko hata watu wa Yazeri. Matawi yako yametanda mpaka ngambo ya bahari ya Chumvi yakafika hata mpaka Yazeri. Lakini mwangamizi ameyakumba matunda yako ya kiangazi na zabibu zako. Furaha na shangwe zimeondolewa kutoka nchi ya Moabu yenye rutuba. Nimeikomesha divai kutoka mashinikizo hakuna mtu anayekamua zabibu kwa shangwe; kelele zinazosikika si za shangwe. “Kilio cha watu wa Heshboni chasikika huko Eleale mpaka Yahazi; kinaenea kutoka Soari mpaka Horonaimu na hata Eglath-shelishiya. Hata maji ya kijito Nimrimu yamekauka. Nami nitamfutilia mbali kila mtu katika Moabu ambaye anatambikia vilimani na kumfukizia ubani mungu wake. “Kwa hiyo, moyo wangu unaomboleza juu ya watu wa Moabu na watu wa Kir-heresi, kama mpiga zumari mazishini; maana hata mali yote waliyojipatia imeangamia. Kila mtu amenyoa upara na ndevu zake. Wote wamejikatakata mikononi na viunoni wamevaa mavazi ya gunia. Juu ya nyumba za Moabu na katika viwanja vyao hakuna kinachosikika ila tu maombolezo. Mimi nimemvunja Moabu kama chombo kisichotakiwa na mtu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Tazama alivyovunjika! Tazama wanavyoomboleza! Ajabu jinsi Moabu alivyorudi nyuma kwa aibu! Moabu amekuwa kichekesho na kioja kwa jirani zake wote.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Tazama, taifa litaruka kasi kuivamia Moabu, kama tai aliyekunjua mabawa yake. Miji yake itatekwa, ngome zitachukuliwa. Siku hiyo mioyo ya wanajeshi wa Moabu, itaogopa kama mwanamke anayejifungua. Wamoabu wataangamizwa, wasiwe tena taifa, kwa sababu walijikweza dhidi ya Mwenyezi-Mungu. Kitisho, mashimo na mtego, vinawasubiri enyi watu wa Moabu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Atakayetoroka kitisho atatumbukia shimoni; atakayetoka shimoni atanaswa mtegoni. Kwa maana nitaleta mambo hayo juu ya Moabu, katika mwaka wao wa adhabu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Wakimbizi wachovu wanatua Heshboni kutaka usalama, maana moto umezuka huko mjini; mwali wa moto toka ikulu ya mfalme Sihoni; umeteketeza mipaka ya Moabu, umeunguza milima yao hao watukutu. Ole wenu watu wa Moabu! Watu wa Kemoshi sasa mmeangamizwa, wana wenu wamechukuliwa mateka, binti zenu wamepelekwa uhamishoni. Lakini siku zijazo nitamstawisha tena Moabu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Hii ndiyo hukumu juu ya Moabu.” Kuhusu Waamoni. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Je, Israeli hana watoto? Je, hana warithi? Mbona basi mungu Milkomu amemiliki Gadi na watu wake kufanya makao yao mijini mwake? Basi, wakati unakuja kweli, siku zaja, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, ambapo nitavumisha sauti ya vita dhidi ya Raba mji wa Waamoni. Raba utakuwa rundo la uharibifu, vijiji vyake vitateketezwa moto; ndipo Israeli atakapowamiliki wale waliomiliki. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Ombolezeni, enyi watu wa Heshboni, maana mji wa Ai umeharibiwa! Lieni enyi binti za Raba! Jifungeni mavazi ya gunia viunoni ombolezeni na kukimbia huko na huko uani! Maana mungu Milkomu atapelekwa uhamishoni, pamoja na makuhani wake na watumishi wake. Mbona mnajivunia mabonde yenu, enyi msioamini, watu mliotegemea mali zenu, mkisema: ‘Nani atathubutu kupigana nasi?’ Basi, mimi nitawaleteeni vitisho kutoka kwa jirani zenu wote, nanyi mtafukuzwa nje kila mtu kivyake, bila mtu wa kuwakusanya wakimbizi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Lakini baadaye nitawarudishia Waamoni fanaka yao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Kuhusu Edomu. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Je, hakuna tena hekima mjini Temani? Je, wenye busara wao hawana shauri tena? Hekima imetoweka kabisa? Kimbieni enyi wakazi wa Dedani; geukeni mkaishi mafichoni! Maana nitawaleteeni maangamizi enyi wazawa wa Esau; wakati wa kuwaadhibu umefika. Wachuma zabibu watakapokuja kwenu hawatabakiza hata zabibu moja. Usiku ule wezi watakapofika, wataharibu kila kitu mpaka watosheke. Lakini nimemnyanganya Esau kila kitu, naam, nimeyafunua maficho yake, wala hawezi kujificha tena. Watoto, ndugu na jirani zake wameangamizwa; hakuna hata mmoja aliyebaki. Niachieni watoto wenu yatima nami nitawatunza; waacheni wajane wenu wanitegemee.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ikiwa wale ambao hawakustahili kunywa kikombe cha adhabu ni lazima wanywe, je, wewe utaachwa bila kuadhibiwa? La! Hutakosa kuadhibiwa; ni lazima unywe hicho kikombe! Maana nimeapa kwa nafsi yangu kwamba mji wa Bosra utakuwa kioja na kichekesho, utakuwa uharibifu na laana; vijiji vyote vitakuwa magofu daima. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Nimepata habari kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, mjumbe ametumwa ayatangazie mataifa: “Jikusanyeni pamoja dhidi ya Edomu; inukeni mwende kuushambulia! Mimi Mwenyezi-Mungu nitakufanya wee Edomu kuwa mdogo kuliko mataifa yote. Ulimwengu wote utakudharau. Vitisho unavyotoa na kiburi chako vimekudanganya, ewe ukaaye katika mapango ya miamba, unayeishi juu ya kilele cha mlima! Ingawa unaweka makao yako juu kama ya tai, mimi nitakuporomosha kutoka huko uliko. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Edomu itakuwa kitisho na kila mtu atakayepita karibu yake atashangaa, na kuizomea kwa sababu ya maafa yatakayoipata. Kama vile Sodoma na Gomora na miji jirani yake ilivyoangamizwa, mimi Mwenyezi-Mungu nasema, hakutakuwa na mtu yeyote atakayeishi Edomu wala kufanya mashauri humo. Kama vile simba anavyochomoza kutoka msitu wa mto Yordani na kuingia kwenye malisho mazuri, ndivyo nitakavyowafukuza ghafla Waedomu kutoka nchi yao. Nami nitamweka huko kiongozi yeyote nitakayemchagua. Maana, ni nani anayeweza kulinganishwa nami? Nani awezaye kunishtaki? Ni mchungaji gani awezaye kunipinga? Kwa hiyo, sikilizeni mpango ambao mimi Mwenyezi-Mungu nimepanga dhidi ya Edomu pamoja na mambo niliyokusudia kuwafanyia wakazi wa Temani: Hakika, watoto wao wadogo wataburutwa na kuchukuliwa; kweli kutakuwa na mshangao mkubwa katika makao yao! Kwa kishindo cha kuanguka kwao, dunia itatetemeka; sauti ya kilio chao itasikika mpaka bahari ya Shamu. Tazama, adui atapanda juu na kuruka kama tai na kutandaza mabawa yake juu ya Bosra. Siku hiyo moyo wa mashujaa wa Edomu utakumbwa na hofu kama ya mwanamke anayejifungua.” Kuhusu Damasko: “Miji ya Hamathi na Arpadi, imejaa wasiwasi kwa kufikiwa na habari mbaya; mioyo ya watu wake inayeyuka kwa hofu, imefadhaika kama bahari isiyoweza kutulia. Watu wa Damasko wamekufa moyo; wamegeuka wapate kukimbia; hofu kubwa imewakumba, uchungu na huzuni vimewapata, kama mwanamke anayejifungua Ajabu kuachwa kwa mji maarufu, mji uliokuwa umejaa furaha! Basi vijana wake wataanguka viwanjani mwake, askari wake wote wataangamizwa siku hiyo. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Nitawasha moto katika kuta za Damasko, nao utateketeza ngome za mfalme Ben-hadadi.” Kuhusu Kedari na falme za Hazori ambazo Nebukadneza mfalme wa Babuloni, alizishambulia na kuzishinda, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Inuka uende kulishambulia kabila la Kedari! Waangamize watu wa mashariki! Hema zao na kondoo wao vitachukuliwa, kadhalika mapazia yao na mali yao yote; watanyanganywa ngamia wao, na kilio kitasikika: ‘Kitisho kila upande!’ Kimbieni, nendeni mbali, kaeni mashimoni. Enyi wakazi wa Haziri, kimbieni mtangetange na kukaa mafichoni! Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Maana Nebukadneza mfalme wa Babuloni, amefanya mpango dhidi yenu, amepania kuja kuwashambulia. Inuka uende kulishambulia taifa linalostarehe, taifa linaloishi kwa usalama. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Taifa hilo halina malango wala pao za chuma; ni taifa ambalo liko peke yake. “Ngamia wao watatekwa mifugo yao itachukuliwa mateka. Nitawatawanya kila upande, watu wale wanaonyoa denge. Nitawaletea maafa kutoka kila upande. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mji wa Hazori utakuwa makao ya mbweha, utakuwa jangwa daima; hakuna mtu atakayekaa humo, wala atakayeishi humo.” Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Elamu, mwanzoni mwa utawala wa Sedekia, mfalme wa Yuda. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, asema hivi: “Nitavunja upinde wa watu wa Elamu ulio msingi wa nguvu zao. Nitaleta upepo kutoka pande zote za mbingu; nitawatawanya kila mahali, wala hapatakuwa na taifa lolote ambalo halitakuwa na wakimbizi wa Elamu. Nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya maadui zao na mbele ya wale wanaotaka kuyaangamiza maisha yao. Nitawaletea maafa na hasira yangu kali. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitawaletea upanga kuwafuata mpaka niwaangamize kabisa. Nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu na kumwangamiza mfalme wao pamoja na wakuu wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Lakini katika siku za mwisho, nitaurudishia mji wa Elamu fanaka yake. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu alilosema kwa njia ya nabii Yeremia kuhusu nchi ya Babuloni na nchi ya Wakaldayo: “Tangazeni kati ya mataifa, twekeni bendera na kutangaza, Msifiche lolote. Semeni: ‘Babuloni umetekwa, Beli ameaibishwa. Merodaki amefadhaishwa; sanamu zake zimeaibishwa, vinyago vyake vimefadhaishwa.’ “Kwa maana, taifa kutoka kaskazini limefika kuushambulia; litaifanya nchi yake kuwa uharibifu. Hakuna atakeyeishi humo; watu na wanyama watakimbia mbali. “Siku hizo na wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, watu wa Israeli na watu wa Yuda watakusanyika pamoja na kurudi wakilia huku wananitafuta mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Watauliza njia ya kwenda Siyoni, huku nyuso zao zimeelekea huko, wakisema, ‘Njoni!’ Nao watajiunga na Mwenyezi-Mungu katika agano la milele ambalo kamwe halitasahauliwa. “Watu wangu walikuwa kondoo waliopotea; wachungaji wao wamewapotosha, wakawageuza kuelekea milimani; walitembea toka mlima hadi kilima, wakasahau zizi lao. Watu wote waliowakuta waliwaua, na maadui zao wamesema, ‘Hatuna hatia sisi’, maana hao wamemkosea Mwenyezi-Mungu aliye malisho yao ya kweli; Mwenyezi-Mungu ambaye ni tegemeo la wazee wao! “Kimbieni kutoka Babuloni! Tokeni nje ya nchi ya Wakaldayo, muwe kama mabeberu mbele ya kundi. Maana, mimi nitachochea mataifa makubwa kutoka nchi ya kaskazini washambulie Babuloni. Watajiandaa kuishambulia Babuloni na kuiteka. Mishale yao ni kama shujaa hodari asiyerudi mikono mitupu. Nchi ya Wakaldayo itaporwa, na hao watakaoipora wataridhika. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Enyi waporaji wa mali yangu! Japo mnafurahi na kushangilia, mnarukaruka kama mtamba wa ng'ombe anayepura nafaka, na kulia kama farasi dume, nchi yenu ya kuzaliwa itaaibishwa; hiyo nchi mama yenu itafedheheshwa. Lo! Babuloni itakuwa ya mwisho kati ya mataifa, itakuwa nyika kame na jangwa. Kwa sababu ya ghadhabu yangu Mwenyezi-Mungu, Babuloni haitakaliwa kabisa na watu, bali itakuwa jangwa kabisa; kila atakayepita karibu nayo atashangaa ataizomea kwa sababu ya majeraha yake. “Enyi nyote wapiga mishale stadi, shikeni nafasi zenu kuuzingira mji wa Babuloni; upigeni, msibakize mshale hata mmoja, maana umenikosea mimi Mwenyezi-Mungu. Upigieni kelele za vita pande zote, sasa Babuloni umejitoa ukamatwe. Ngome zake zimeanguka, kuta zake zimebomolewa. Ninalipiza kisasi juu ya Babuloni Basi jilipizeni kisasi, utendeeni kama ulivyowatenda wengine. Zuieni watu wasipande mbegu Babuloni, wala wasivune wakati wa mavuno. Kutokana na upanga wa udhalimu, kila mmoja atawarudia watu wake kila mmoja atakimbilia nchini mwake. “Israeli ni kondoo wanaowindwa na kufukuzwa na simba. Kwanza waliangamizwa na mfalme wa Ashuru, na sasa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, amevunjavunja mifupa yake. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nitamwadhibu mfalme wa Babuloni na nchi yake, kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru. Nitawarudisha Waisraeli nchini mwao, nao watakula mavuno yatakayolimwa juu ya mlima Karmeli na Bashani na watatosheka kwa chakula kutoka milima ya Efraimu na Gileadi. Siku hizo na wakati huo, uovu utatafutwa nchini Israeli, lakini hautapatikana; dhambi itatafutwa nchini Yuda, lakini haitapatikana; maana mimi nitawasamehe wale ambao nimewabakiza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Pandeni, mwiendee nchi ya Merathaimu, nendeni kuishambulia; washambulieni wakazi wa Pekodi na kuwaangamiza kabisa watu wake. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Fanyeni kila kitu nilichowaamuru. Kelele za vita zinasikika nchini, kuna uharibifu mkubwa. Jinsi gani huo mji uliokuwa nyundo ya dunia nzima unavyoangushwa chini na kuvunjika! Babuloni umekuwa kinyaa miongoni mwa mataifa! Ewe Babuloni, nilikutegea mtego ukanaswa, wala hukujua juu yake; ulipatikana, ukakamatwa, kwa sababu ulishindana nami Mwenyezi-Mungu. Nimefungua ghala yangu ya silaha, nikatoa humo silaha za ghadhabu yangu, maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nina kazi ya kufanya katika nchi ya Wakaldayo. Njoni mkamshambulie kutoka kila upande; zifungueni ghala zake za chakula; mrundikieni marundo ya nafaka! Iangamizeni kabisa nchi hii; msibakize chochote! Waueni askari wake hodari; waache washukie machinjoni. Ole wao, maana siku yao imewadia, wakati wao wa kuadhibiwa umefika. “Sikiliza! Wakimbizi na watoro kutoka nchi ya Babuloni wanakuja kutangaza huko Siyoni jinsi Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyolipiza kisasi kwa ajili ya hekalu lake. “Waiteni wapiga mishale waishambulie Babuloni. Pelekeni kila mtu ajuaye kuvuta upinde. Uzingireni mji pasiwe na yeyote atakayetoroka. Ulipizeni kadiri ya matendo yake yote; utendeeni kama ulivyowatendea wengine, maana kwa kiburi ulinidharau mimi Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli. Kwa hiyo, vijana wake watauawa katika mitaa yake, na majeshi yake yote yataangamizwa siku hiyo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, napigana nawe ewe mwenye kiburi, maana siku yako ya adhabu imefika, wakati nitakapokuadhibu umewadia. Mwenye kiburi atajikwaa na kuanguka, wala hapatakuwa na mtu wa kumwinua. Nitawasha moto katika miji yake, nao utateketeza kila kitu kandokando yake.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Watu wa Israeli wanakandamizwa; hali kadhalika na watu wa Yuda. Wale waliowachukua mateka wamewabana sana na wanakataa kuwaachia. Lakini mimi, Mkombozi wao ni mwenye nguvu. Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina langu. Hakika nitatetea kisa chao ili nilete amani katika nchi yao, lakini taabu kwa wakazi wa Babuloni. “Kifo kwa Wakaldayo, kwa wakazi wa Babuloni na maofisa na wenye hekima wake! Kifo kwa waaguzi, wanachotangaza ni upumbavu tu! Kifo kwa mashujaa wake, ili waangamizwe! Kifo kwa farasi wake na uharibifu kwa magari yake, kifo kwa majeshi yake yote ya kukodiwa, ili wawe na woga kama wanawake! Uharibifu kwa hazina zake zote ili zipate kuporwa. Ukame uyapate maji ili yapate kukauka! Maana Babuloni ni nchi ya sanamu za miungu, watu ni wendawazimu juu ya vinyago vyao. “Kwa hiyo wanyama wa porini, mbwamwitu pamoja na mbuni, watakaa Babuloni. Hapatakaliwa kamwe na watu vizazi vyote vijavyo. Kama vile mimi Mwenyezi-Mungu nilivyoiangamiza miji ya Sodoma na Gomora na miji ya jirani, vivyo hivyo hapatakuwa na mtu yeyote atakayeishi humo. Naam, hakuna mtu yeyote atakeyekaa huko. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Tazama! Watu wanakuja kutoka kaskazini; taifa lenye nguvu na wafalme wengi wanajitayarisha kutoka miisho ya dunia. Wameshika pinde zao na mikuki; ni watu wakatili na wasio na huruma. Vishindo vyao ni kama mvumo wa bahari, wamepanda farasi. Wamejipanga tayari kwa vita, dhidi yako wewe Babuloni! Mfalme wa Babuloni amesikia habari zao, nayo mikono yake ikawa kama kamba. Ameshikwa na dhiki na uchungu kama mama anayejifungua. “Tazama, mimi nitakuwa kama simba anayechomoza kutoka msitu wa mto Yordani na kuingia kwenye malisho mazuri: Mimi Mwenyezi-Mungu nitawafukuza ghafla watu wake kutoka kwake. Nami nitamweka huko kiongozi yeyote nitakayemchagua. Maana, ni nani anayeweza kulinganishwa nami? Nani awezaye kunishtaki? Ni mchungaji gani awezaye kunipinga? Kwa hiyo, sikilizeni mpango ambao mimi Mwenyezi-Mungu nimepanga dhidi ya Babuloni pamoja na mambo niliyokusudia kuitendea nchi ya Wakaldayo: Hakika watoto wao wataburutwa na kuchukuliwa; kweli kutakuwa na mshangao mkubwa katika makao yao. Kwa kishindo cha kutekwa kwa Babuloni dunia itatetemeka, na kilio chake kitasikika miongoni mwa mataifa mengine.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nitachochea upepo wa kuangamiza dhidi ya Babuloni, dhidi ya wakazi wa Kaldayo. Nitawapeleka wapepetaji Babuloni, nao watampepeta; watamaliza kila kitu katika nchi yake watakapofika kuishambulia toka kila upande wakati wa maangamizi yake.” Usiwape nafasi wapiga mshale wa Babuloni; usiwaache wavute upinde, wala kuvaa mavazi yao ya vita. Usiwahurumie vijana wake; liangamize kabisa jeshi lake. Wataanguka na kuuawa katika nchi ya Wakaldayo, watajeruhiwa katika barabara zake. Lakini Israeli na Yuda hawakuachwa na Mungu wao Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ingawa nchi yao imejaa hatia mbele yake yeye Mtakatifu wa Israeli. Kimbieni kutoka Babuloni, kila mtu na ayaokoe maisha yake! Msiangamizwe katika adhabu yake, maana huu ndio wakati wa Mungu wa kulipa kisasi, anaiadhibu Babuloni kama inavyostahili. Babuloni ilikuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa Mwenyezi-Mungu, ambacho kiliilewesha dunia nzima. Mataifa yalikunywa divai yake, hata yakapatwa wazimu. Ghafla Babuloni imeanguka na kuvunjikavunjika; ombolezeni kwa ajili yake! Leteni dawa kutuliza maumivu yake; labda utaweza kuponywa. Tulijaribu kuuponya Babuloni, lakini hauwezi kuponywa. Uacheni, twendeni zetu, kila mmoja katika nchi yake, maana hukumu yake ni kuu mno imeinuka mpaka mawinguni. Mwenyezi-Mungu amethibitisha kuwa hatuna hatia. Twendeni Siyoni tukatangaze matendo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Mwenyezi-Mungu amezichochea roho za wafalme wa Media, kwa maana amenuia kuiangamiza Babuloni. Naam, hicho ndicho kisasi cha Mwenyezi-Mungu; analipiza kisasi kwa ajili ya hekalu lake. Noeni mishale yenu! Chukueni ngao! Twekeni bendera ya vita kushambulia kuta za Babuloni. Imarisheni ulinzi; wekeni walinzi; tayarisheni mashambulizi. Mwenyezi-Mungu amepanga na kutekeleza mambo aliyosema juu ya wakazi wa Babuloni. Nchi hiyo imejaa mito na hazina tele, lakini mwisho wake umefika, uzi wa uhai wake umekatwa. Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameapa kwa nafsi yake: “Hakika nitakujaza majeshi mengi kama nzige, nayo yatapiga vigelegele vya ushindi juu yako” Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeumba dunia kwa nguvu yake, aliyeuimarisha ulimwengu kwa hekima yake, na kwa maarifa yake akazitandaza mbingu. Anapotoa sauti yake maji hutitima mbinguni, hufanya ukungu upande kutoka mipaka ya dunia. Hufanya umeme umulike wakati wa mvua huvumisha upepo kutoka ghala zake. Kila mtu ni mpumbavu bila maarifa, kila mhunzi anaaibishwa na vinyago vyake; maana sanamu zake ni udanganyifu mtupu, wala hazina pumzi ndani yake. Hazina thamani, ni udanganyifu mtupu; wakati watakapoadhibiwa, nazo zitaangamia. Mungu aliye hazina ya Yakobo si kama hizo, maana yeye ndiye aliyeviumba vitu vyote, na Israeli ni kabila lililo mali yake; Mwenyezi-Mungu wa Majeshi, ndilo jina lake. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wewe Babuloni ni rungu na silaha yangu ya vita; nakutumia kuyavunjavunja mataifa, nakutumia kuangamiza falme. Nakutumia kuponda farasi na wapandafarasi, magari ya kukokotwa na waendeshaji wake. Ninakutumia kuwaponda wanaume na wanawake, wazee na vijana, wavulana na wasichana. Ninakutumia kuponda wachungaji na makundi yao, wakulima na wanyama wao wa kulimia, wakuu wa mikoa na madiwani. “Nitaiadhibu Babuloni na wakazi wote wa Kaldayo mkiona kwa macho yenu wenyewe, kwa sababu ya uovu wote walioufanya katika Siyoni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mimi ninapingana nawe ewe mlima mharibifu, mlima unaoharibu dunia nzima! Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Nitanyosha mkono wangu dhidi yako, nitakuangusha kutoka miambani juu na kukufanya kuwa mlima uliochomwa moto; hata hamna jiwe lako litakalochukuliwa kujengea, hakuna jiwe litakalochukuliwa kuwekea msingi! Utakuwa kama jangwa milele. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Tweka bendera ya vita duniani, piga tarumbeta kati ya mataifa; yatayarishe mataifa kupigana naye; ziite falme kuishambulia; falme za Ararati, Mini na Ashkenazi. Weka majemadari dhidi yake; walete farasi kama makundi ya nzige. Yatayarishe mataifa kupigana naye vita; watayarishe wafalme wa Medi, watawala na mawakili wao, tayarisheni nchi zote katika himaya yake. Nchi inatetemeka na kugaagaa kwa maumivu, maana nia ya Mwenyezi-Mungu kuhusu Babuloni ni thabiti: Ataifanya nchi ya Babuloni kuwa jangwa, ataifanya iwe bila watu. Askari wa Babuloni wameshindwa kupigana, wamebaki katika ngome zao; nguvu zao zimewaishia, wamekuwa kama wanawake. Nyumba za Babuloni zimechomwa moto, malango yake ya chuma yamevunjwa. Tarishi baada ya tarishi wanapiga mbio, mjumbe mmoja anamfuata mjumbe mwingine, kumpasha habari mfalme wa Babuloni kwamba mji wake umevamiwa kila upande. Vivuko vya mto vimetekwa, ngome zimechomwa moto, askari wamekumbwa na hofu. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli asema hivi: “Babuloni ni kama uwanja wa kupuria nafaka wakati unapotayarishwa. Lakini bado kidogo tu, wakati wa mavuno utaufikia.” Mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliuharibu na kuuponda mji wa Yerusalemu aliuacha kama chungu kitupu; aliumeza kama joka. Alijaza tumbo lake vitu vyake vizurivizuri, akautupilia mbali kama matapishi. Watu wa Yerusalemu na waseme: “Babuloni na ulipizwe ukatili uleule, tuliotendwa sisi pamoja na jamaa zetu! Babuloni ipatilizwe kwa umwagaji wa damu yetu.” Kwa hiyo asema hivi Mwenyezi-Mungu: “Nitawatetea kuhusu kisa chenu, na kulipiza kisasi kwa ajili yenu. Nitaikausha bahari ya Babuloni na kuvifanya visima vyake vikauke. Babuloni itakuwa rundo la magofu, itakuwa makao ya mbweha, itakuwa kinyaa na kitu cha kuzomewa; hakuna mtu atakayekaa huko. Wababuloni watanguruma pamoja kama simba; watakoroma kama wanasimba. Wakiwa na uchu mkubwa nitawaandalia karamu: Nitawalewesha mpaka wapepesuke; nao watalala usingizi wa daima na hawataamka tena. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitawashusha chini kama kondoo wa kuchinjwa, kama vile kondoo dume na beberu. Ajabu kutekwa kwa Babuloni; mji uliosifika duniani kote umechukuliwa! Babuloni umekuwa kinyaa kati ya mataifa! Bahari imefurika juu ya Babuloni, Babuloni imefunikwa mawimbi yaliyochafuka. Miji yake imekuwa kinyaa, nchi ya ukavu na jangwa, nchi isiyokaliwa na mtu yeyote, wala kupitika na binadamu yeyote. Nitamwadhibu mungu Beli huko Babuloni, nitamfanya akitoe alichokimeza. Mataifa hayatamiminika tena kumwendea. Ukuta wa Babuloni umebomoka. “Tokeni humo enyi watu wangu! Kila mtu na ayasalimishe maisha yake, kutoka hasira kali ya Mwenyezi-Mungu. Msife moyo wala msiwe na hofu, kwa sababu ya uvumi mnaosikia nchini. Mwaka huu kuna uvumi huu, mwaka mwingine uvumi mwingine; uvumi wa ukatili katika nchi, mtawala mmoja dhidi ya mtawala mwingine. Kweli siku zaja, nitakapoadhibu sanamu za Babuloni; nchi yake yote itatiwa aibu, watu wake wote watauawa humohumo. Kisha mbingu, dunia na vyote vilivyomo vitaimba kwa furaha kuhusu kuanguka kwa Babuloni, waangamizi watakapofika kutoka kaskazini kuushambulia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Babuloni umesababisha vifo duniani kote; sasa wenyewe utaangamizwa kwa mauaji ya Israeli. “Nyinyi mlinusurika kifo, ondokeni sasa, wala msisitesite! Ingawa mko nchi ya mbali mkumbukeni Mwenyezi-Mungu, ukumbukeni pia mji wa Yerusalemu. Mnasema: ‘Tumeaibishwa na kufadhaishwa; aibu imezifunika nyuso zetu, kwa sababu wageni wameingia katika sehemu takatifu za nyumba ya Mwenyezi-Mungu.’ “Kwa hiyo, wakati unakuja, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, ambapo nitaviadhibu vinyago vya Babuloni, na majeruhi watapiga kite katika nchi yake yote. Ingawa Babuloni atapanda mpaka mbinguni, na kuziimarisha ngome zake ndefu, waangamizi watakuja kutoka kwangu kumvamia. 2Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Sikiliza! Kilio kinasikika kutoka Babuloni! Kishindo cha maangamizi makubwa kutoka nchi ya Wakaldayo! Maana mimi Mwenyezi-Mungu naiangamiza Babuloni, na kuikomesha kelele yake kubwa. Adui ananguruma kama mawimbi ya maji mengi, sauti ya kishindo chao inaongezeka. Naam, mwangamizi anaijia Babuloni; askari wake wametekwa, pinde zao zimevunjwavunjwa. Mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu mwenye kuadhibu, hakika mimi nitalipiza kisasi kamili. Nitawalewesha wakuu na wenye hekima wake, watawala wake, madiwani na askari wake; watalala usingizi wa milele wasiinuke tena. Nasema mimi mfalme ambaye jina langu ni Mwenyezi-Mungu wa Majeshi. “Mimi Mwenyezi-Mungu wa Majeshi nasema: Ukuta mpana wa Babuloni utabomolewa mpaka chini, na malango yake marefu yatateketezwa kwa moto. Watu wanafanya juhudi za bure, mataifa yanajichosha maana mwisho wao ni motoni!” Mnamo mwaka wa nne wa utawala wake, mfalme Sedekia alikwenda Babuloni pamoja na ofisa wa askari wake aitwaye Seraya mwana wa Neria na mjukuu wa Maseya. Kutokana na fursa hiyo mimi Yeremia nilimpa Seraya ujumbe. Nilikuwa nimeandika kitabuni maafa yote niliyotangaza juu ya Babuloni na pia maneno mengine kuhusu Babuloni. Nilimwambia Seraya: “Utakapofika Babuloni ni lazima uwasomee wote ujumbe huu. Kisha umalizie na maneno haya: ‘Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umesema kwamba utapaharibu mahali hapa hata pasikaliwe na kiumbe chochote, mwanadamu au mnyama, na kwamba nchi hii itakuwa jangwa milele.’ Utakapomaliza kusoma kitabu hiki, kifungie jiwe, kisha ukitumbukize katikati ya mto Eufrate, ukisema: ‘Hivi ndivyo mji wa Babuloni utakavyozama, wala hautainuka tena, kwa sababu ya maafa ambayo Mwenyezi-Mungu anauletea.’” Mwisho wa maneno ya Yeremia. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, mkazi wa mji wa Liba. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama mabaya yote aliyotenda Yehoyakimu. Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia sana watu wa Yerusalemu na Yuda hata akawafukuza mbali naye. Sedekia alimwasi mfalme wa Babuloni. Ikawa katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, mwaka wa tisa wa kutawala kwake Sedekia, Nebukadneza mfalme wa Babuloni, alifika na jeshi lake lote kuushambulia Yerusalemu, wakauzingira kila upande. Mji uliendelea kuzingirwa mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia. Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ilikuwa kali sana mjini hata hapakuwa na chakula chochote kwa ajili ya wakazi wake. Basi, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa, nao askari walikimbia wakatoka nje ya mji wakati wa usiku wakipitia njia ya lango katikati ya kuta mbili, kwenye bustani ya mfalme, wakaenda upande wa Araba, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji wote. Waisraeli walikimbia kuelekea bonde la mto Yordani. Lakini jeshi la Wakaldayo lilimfuatia mfalme na kumteka katika tambarare za Yeriko, jeshi lake lote likatawanyika na kumwacha. Basi Wakaldayo walimteka mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babuloni, huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, naye akamhukumu. Hukohuko Ribla, mfalme wa Babuloni aliwaua wana wa Sedekia mbele ya baba yao. Aliwaua pia maofisa wote wa Yuda. Kisha aliyangoa macho ya Sedekia na kumfunga pingu, akamchukua Sedekia Babuloni na kumtia kizuizini mpaka siku alipokufa. Katika siku ya kumi ya mwezi wa tano, mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme ambaye alimtumikia mfalme wa Babuloni, aliingia Yerusalemu. Alichoma moto nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu na nyumba zote za Yerusalemu; kila nyumba kubwa ilichomwa moto. Askari wote wa Wakaldayo waliokuwa pamoja na kapteni wa walinzi, walizibomoa kuta zote zilizouzunguka mji wa Yerusalemu. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwachukua uhamishoni watu waliokuwa wamebakia mjini na wale waliokuwa wamejisalimisha kwa mfalme wa Babuloni pamoja na mafundi. Lakini Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwaacha baadhi ya watu waliokuwa maskini kabisa nchini, wawe watunza mizabibu na wakulima. Wakaldayo walivunja vipandevipande nguzo za shaba nyeusi ambazo zilikuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu pamoja na vikalio na birika kubwa la shaba nyeusi lililokuwamo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaichukua shaba nyeusi yote mpaka Babuloni. Kadhalika, walichukua vyungu, sepetu, mikasi, makarai, vijiko vikubwa na vyombo vyote vya shaba nyeusi vilivyotumiwa katika huduma ya hekalu. Pia kapteni wa walinzi wa mfalme alichukua vibakuli, vyetezo, mabirika, vyungu, vinara vya taa, vijiko vikubwa na mabakuli ya sadaka za vinywaji, vyombo hivyo vikiwa vya dhahabu au vya fedha. Kuhusu vitu Solomoni alivyotengeneza: Nguzo mbili, birika kubwa moja na sanamu za fahali kumi na mbili za shaba nyeusi ambazo zilikuwa chini ya hilo birika kubwa pamoja na vikalio, shaba nyeusi ya vitu hivi vyote ilikuwa na uzito mwingi sana. Kila moja ya nguzo hizo mbili ilikuwa na urefu wa mita 8, mzingo wake mita 5.25, na unene wa milimita 75, zote zilikuwa wazi ndani. Juu ya kila nguzo kulikuwa na kichwa cha shaba nyeusi; urefu wa kila kichwa ulikuwa mita 2 na sentimita 20. Kila kichwa kilizungushiwa mapambo ya wavu ya makomamanga, yote ya shaba nyeusi. Kulikuwa na makomamanga tisini na sita ubavuni mwa nguzo hizo; jumla ya makomamanga yote ilikuwa 100 na mapambo kandokando yake. Kisha Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, alimchukua mateka Seraya kuhani mkuu, na Sefania kuhani wa pili, pamoja na walinda mlango watatu; na kutoka mjini alimchukua ofisa mmoja ambaye alikuwa akiongoza askari vitani, pamoja na watu saba washauri wa mfalme ambao aliwakuta mjini. Kadhalika alimchukua katibu wa kamanda mkuu wa jeshi ambaye alitunza kumbukumbu za jeshi pamoja na watu mashuhuri sitini ambao aliwakuta mjini Yerusalemu. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwachukua watu hao na kuwapeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliwapiga na kuwaua watu hao huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Basi, watu wa Yuda walikwenda uhamishoni nje ya nchi yao. Ifuatayo ni idadi ya watu ambao Nebukadneza aliwachukua uhamishoni mnamo mwaka wa saba wa utawala wake: Alichukua Wayahudi 3,023; mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, alichukua kutoka Yerusalemu mateka 832; mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake Nebukadneza, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, alichukua mateka Wayahudi 745. Jumla ya mateka wote ilikuwa watu 4,600. Mnamo mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda alipopelekwa uhamishoni, siku ya ishirini na tano ya mwezi wa kumi na mbili, Evil-merodaki mfalme wa Babuloni, mwaka uleule alipofanywa mfalme, alimsamehe Yehoyakini mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani. Aliongea naye vizuri na kumpa nafasi ya heshima kuliko wafalme wengine waliokuwa pamoja naye uhamishoni huko Babuloni. Basi, Yehoyakini alibadili mavazi yake ya kifungoni, akawa anapata chakula chake daima mezani kwa mfalme. Daima alipewa posho na mfalme wa Babuloni kulingana na mahitaji yake ya kila siku, mpaka alipofariki. Ajabu mji uliokuwa umejaa watu, sasa wenyewe umebaki tupu! Ulikuwa maarufu kati ya mataifa; sasa umekuwa kama mama mjane. Miongoni mwa miji ulikuwa kama binti mfalme; sasa umekuwa mtumwa wa wengine. Walia usiku kucha; machozi yautiririka. Hakuna hata mmoja wa wapenzi wake wa kuufariji. Rafiki zake wote wameuhadaa; wote wamekuwa adui zake. Watu wa Yuda wamekwenda uhamishoni pamoja na mateso na utumwa mkali. Sasa wanakaa miongoni mwa watu wa mataifa, wala hawapati mahali pa kupumzika. Waliowafuatia wamewakamata wakiwa taabuni. Barabara za kwenda Siyoni zinasikitisha; hakuna wapitao kwenda kwenye sikukuu. Malango ya mji wa Siyoni ni tupu; makuhani wake wanapiga kite, wasichana wake wana huzuni, na mji wenyewe uko taabuni. Adui zake ndio wanaoutawala na wanafanikiwa, kwani Mwenyezi-Mungu ameutesa kwa sababu ya makosa mengi. Watoto wake wametekwa na kupelekwa mbali. Fahari yote ya watu wa Siyoni imewatoweka; wakuu wake wamekuwa kama kulungu wasio na malisho. Bila nguvu waliwakimbia watesi wao. Ukiwa sasa magofu matupu, Yerusalemu wakumbuka fahari yake. Ulipoangukia mikononi mwa maadui zake, hakuna aliyekuwako kuusaidia. Washindi wake walichekelea kuanguka kwake. Yerusalemu ulitenda dhambi mbaya, ukawa mchafu kwa dhambi zake. Wote waliousifia wanaudharau, maana wameuona uchi wake. Wenyewe wapiga kite na kujificha kwa aibu. Uchafu wake ulionekana waziwazi, lakini wenyewe haukujali mwisho wake. Anguko lake lilikuwa kubwa mno; hakuna awezaye kuufariji. Wasema: “Tazama ee Mwenyezi-Mungu mateso yangu, maana adui yangu ameshinda.” Maadui wamenyosha mikono yao, wanyakue vitu vyake vyote vya thamani. Naam umeona watu wa mataifa wakiingia hekaluni, watu ambao Mwenyezi-Mungu aliwakataza kujumuika na jumuiya ya watu wake. Watu wa Yerusalemu wote wanahangaika kutafuta chakula; hazina zao wanazitoa kupata chakula, wajirudishie nguvu zao. Nao mji unalia, “Hebu niangalie, ee Mwenyezi-Mungu, ona jinsi nilivyogeuka kuwa duni. “Enyi wapita njia, hivi hamjali kitu? Tazameni! Hakuna aliyepatwa na uchungu kama mimi, uchungu alioniletea Mwenyezi-Mungu, siku ya hasira yake kali. “Aliteremsha moto kutoka juu, ukanichoma hata mifupani mwangu. Alinitegea wavu akaninasa, kisha akanirudisha nyuma, akaniacha nimeduwaa na kuzirai mchana kutwa. “Aliyahesabu makosa yangu yote akayakusanya mahali pamoja; aliyafunga shingoni mwangu kama nira, nikafyonzwa nguvu zangu kwa uzito wake. Mwenyezi-Mungu aliniweka mikononi mwao watu ambao siwezi kuwapinga. “Mwenyezi-Mungu aliwakataa askari walionilinda, alitangaza wakati maalumu wa kuniadhibu kuwaponda vijana wangu wa kiume. Aliwaponda kama katika shinikizo watu wangu wa Yuda. “Kwa sababu ya hayo ninalia, machozi yanitiririka, sina mtu yeyote wa kunifariji; hakuna yeyote wa kunitia moyo. Watoto wangu wameachwa wakiwa, maana adui yangu amenishinda. “Nainyosha mikono yangu lakini hakuna wa kunifariji. Mwenyezi-Mungu ametoa amri dhidi yangu mimi Yakobo, jirani zangu wawe maadui zangu. Naam, mimi Yerusalemu nimekuwa kinyaa kwao. “Lakini Mwenyezi-Mungu amefanya sawa kwa maana nimeliasi neno lake. Nisikilizeni enyi watu wote, yatazameni mateso yangu. Wasichana wangu na wavulana wangu, wamechukuliwa mateka. “Niliwaita wapenzi wangu, lakini wao wakanihadaa. Makuhani na wazee wangu wamefia mjini wakijitafutia chakula, ili wajirudishie nguvu zao. “Ona, ee Mwenyezi-Mungu nilivyo taabuni. Roho yangu imechafuka, moyo wangu unasononeka kwani nimekuasi vibaya. Huko nje kumejaa mauaji, ndani nako ni kama kifo tu. “Sikiliza ninavyopiga kite; hakuna wa kunifariji. Maadui zangu wote wamesikia juu ya taabu yangu: Wanafurahi kwamba umeniletea maafa. Uifanye ile siku uliyoahidi ifike, uwafanye nao wateseke kama mimi. “Uwapatilize kwa ajili ya uovu wao wote. Uwatende kama ulivyonitenda mimi kwa sababu ya makosa yangu yote. Nasononeka sana kwa maumivu na moyo wangu unazimia.” Mwenyezi-Mungu, kwa hasira yake, amewaweka watu wa Siyoni gizani. Fahari ya Israeli ameibwaga chini. Siku ya hasira yake alilitupilia mbali hata hekalu lake. Mwenyezi-Mungu ameharibu bila huruma makazi yote ya wazawa wa Yakobo. Kwa ghadhabu yake amezibomoa ngome za watu wa Yuda. Ufalme wao na watawala wake ameuporomosha chini kwa aibu. Nguvu yote ya Israeli ameivunja kwa hasira. Hakunyosha mkono kuwasaidia walipokutana na adui; amewawakia watu wa Yakobo kama moto, akateketeza kila kitu. Amevuta upinde wake kama adui, na kuuweka mkono wake wa kulia tayari, amewaua wote tuliowaonea fahari katika maskani yetu watu wa Siyoni. Ametumiminia hasira yake kama moto. Mwenyezi-Mungu amekuwa kama adui, ameangamiza watu wa Israeli; majumba yake yote ameyaharibu, ngome zake amezibomoa. Amewazidishia watu wa Yuda matanga na maombolezo. Hekalu lake amelibomoa kama kitalu bustanini, maskani yake ameiharibu. Amefutilia mbali sikukuu na Sabato huko Siyoni, kwa hasira yake kuu amewakataa mfalme na makuhani. Mwenyezi-Mungu ameipuuza madhabahu yake na hekalu lake amelikataa. Kuta za majumba mjini amewaachia maadui wazibomoe, wakapiga kelele humo nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu kama kelele za wakati wa sikukuu. Mwenyezi-Mungu alipania kuubomoa ukuta wa mji wa Siyoni; aliupima na kuhakikisha kila kitu kimeharibiwa; minara na kuta za nje ya mji akazifanya ukiwa, zote kwa pamoja zikaangamia. Malango yake yameanguka chini, makomeo yake ameyaharibu na kuyavunjavunja. Mfalme na wakuu wake wako uhamishoni kati ya mataifa. Mwongozo wa sheria umetoweka kabisa, manabii wake hawapati tena maono kutoka kwake Mwenyezi-Mungu. Wazee wa Siyoni wameketi chini kimya, wamejitia mavumbi vichwani na kuvaa mavazi ya gunia. Wasichana wa Yerusalemu wameinamisha vichwa. Macho yangu yamevimba kwa kulia, roho yangu imechafuka. Moyo wangu una huzuni nyingi kwa sababu ya kuangamizwa kwa watu wangu kwa sababu watoto wachanga wanazirai katika barabara za mji. Wanawalilia mama zao: “Wapi chakula, wapi kinywaji?” Huku wanazirai kama majeruhi katika barabara za mjini, na kukata roho mikononi mwa mama zao. Nikuambie nini ee Yerusalemu? Nikulinganishe na nini? Nikufananishe na kitu gani ili niweze kukufariji, ee Siyoni uliye mzuri? Maafa yako ni mengi kama bahari. Ni nani awezaye kukuponya? Manabii wako wamekuonea maono madanganyifu, hawakufichua wazi uovu wako ili wapate kukurekebisha, bali walikuonea kauli ya uongo na ya kupotosha. Wapita njia wote wanakudhihaki; wanakuzomea, ee Yerusalemu, wakitikisa vichwa vyao kwa dharau na kusema: “Je, huu ndio ule mji uliofikia upeo wa uzuri, mji uliokuwa furaha ya dunia nzima?” Maadui zako wote wanakuzomea, wanakufyonya na kukusagia meno, huku wakisema, “Tumemwangamiza! Kweli, siku ile tuliyoingojea kwa hamu sasa imefika na tumeiona!” Mwenyezi-Mungu amefanya yale aliyokusudia, ametekeleza yale aliyotishia; kama alivyopanga tangu kale ameangamiza bila huruma yoyote; amewafanya maadui wafurahie adhabu yako, amewakuza mashujaa wa maadui zako. Kuta zako, ee mji wa Siyoni, zimlilie Mwenyezi-Mungu! Machozi na yatiririke kama mto mchana na usiku! Lia na kuomboleza bila kupumzika! Usiku kucha uamkeamke ukalie. Mfungulie Mwenyezi-Mungu yaliyo moyoni mwako. Mwinulie mikono yako kuwaombea watoto wako, watoto wanaozirai kwa njaa popote barabarani. Tazama ee Mwenyezi-Mungu uone! Je, kuna yeyote uliyemtendea ulivyotutendea sisi? Je, hata kina mama wawale watoto wao? Je, nao makuhani wauawe hekaluni mwako? Maiti za vijana na wazee zimelala vumbini barabarani, wasichana na wavulana wangu wameuawa kwa upanga; umewaua bila huruma siku ya hasira yako. Umewaalika kama kwenye sikukuu maadui zangu walionitisha kila upande. Katika siku ya hasira yako ee Mwenyezi-Mungu, hakuna aliyetoroka au kunusurika. Wale niliowazaa na kuwalea adui zangu wamewaangamiza. Mimi ni mtu niliyepata mateso kwa fimbo ya ghadhabu yake Mungu. Amenichukua akanipeleka mpaka gizani kusiko na mwanga. Amenyosha mkono wake dhidi yangu mimi tu, akanichapa tena na tena mchana kutwa. Amenichakaza ngozi na nyama, mifupa yangu ameivunja. Amenizingira na kunizungushia uchungu na mateso. Amenikalisha gizani kama watu waliokufa zamani. Amenizungushia ukuta nisitoroke, amenifunga kwa minyororo mizito. Ingawa naita na kulilia msaada anaizuia sala yangu isimfikie. Njia zangu ameziziba kwa mawe makubwa amevipotosha vichochoro vyangu. Yeye ni kama dubu anayenivizia; ni kama simba aliyejificha. Alinifukuza njiani mwangu, akanilemaza na kuniacha mkiwa. Aliuvuta upinde wake, akanilenga mshale wake. Alinichoma moyoni kwa mishale, kutoka katika podo lake. Nimekuwa kitu cha dhihaka kwa watu wote, mchana kutwa nimekuwa mtu wa kuzomewa. Amenijaza taabu, akanishibisha uchungu. Amenisagisha meno katika mawe, akanifanya nigaegae majivuni. Moyo wangu haujui tena amani, kwangu furaha ni kitu kigeni. Nimewaza “Nimekata tamaa kabisa, tumaini langu kwa Mwenyezi-Mungu limetoweka.” Kukumbuka taabu na kutangatanga kwangu kwanipa uchungu kama wa nyongo. Nayafikiria hayo daima, nayo roho yangu imejaa majonzi. Lakini nakumbuka jambo hili moja, nami ninalo tumaini: Kwamba fadhili za Mwenyezi-Mungu hazikomi, huruma zake hazina mwisho. Kila kunapokucha ni mpya kabisa, uaminifu wake ni mkuu mno. Mwenyezi-Mungu ndiye hazina yangu hivyo nitamwekea tumaini langu. Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wanaomtegemea, ni mwema kwa wote wanaomtafuta. Ni vema mtu kungojea kwa saburi ukombozi utokao kwa Mwenyezi-Mungu. Ni vema mtu kujifunza uvumilivu tangu wakati wa ujana wake. Heri kukaa peke na kimya, mazito yanapompata kutoka kwa Mungu. Yampasa kuinama na kujinyenyekesha, huenda ikawa tumaini bado lipo. Yampasa kumgeuzia shavu mwenye kumpiga, na kuwa tayari kupokea matusi yake. Mwenyezi-Mungu hatatutupa milele. Ingawa atufanya tuhuzunike, atakuwa na huruma tena kadiri ya wingi wa fadhili zake. Yeye hapendelei kuwatesa wala kuwahuzunisha wanadamu. Wafungwa wote nchini wanapodhulumiwa na kupondwa; haki za binadamu zinapopotoshwa mbele yake Mungu Mkuu, kesi ya mtu inapopotoshwa mahakamani, je, Mwenyezi-Mungu haoni hayo? Nani awezaye kuamuru kitu kifanyike Mwenyezi-Mungu asipopanga iwe hivyo? Maafa na mema hutokea tu kwa amri yake Mungu Mkuu. Kwa nini mtu anung'unike, ikiwa ameadhibiwa kwa dhambi zake? Na tupime na kuchunguza mwenendo wetu, tupate kumrudia Mwenyezi-Mungu. Tumfungulie Mungu huko mbinguni mioyo yetu na kumwomba: “Sisi tulikukosea na kukuasi nawe bado hujatusamehe. “Umejizungushia hasira yako ukatufuatia, ukatuua bila huruma. Umejizungushia wingu zito, sala yeyote isiweze kupenya humo. Umetufanya kuwa takataka na uchafu miongoni mwa watu wa mataifa. “Maadui zetu wote wanatuzomea. Kitisho na hofu vimetuandama, tumepatwa na maafa na maangamizi. Macho yangu yabubujika mito ya machozi kwa sababu ya kuangamizwa kwa watu wangu. “Machozi yatanitoka bila kikomo, mpaka Mwenyezi-Mungu kutoka huko mbinguni aangalie chini na kuona. Nalia na kujaa majonzi, kuona yaliyowapata kina mama wa mji wangu. “Nimewindwa kama ndege na hao wanichukiao bila sababu. Walinitupa shimoni nikiwa hai na juu yangu wakarundika mawe. Maji yalianza kunifunika kichwa, nami nikafikiri, ‘Huu ni mwisho wangu.’ “Kutoka chini shimoni nilikulilia ee Mwenyezi-Mungu. Wewe umenisikia nikikulilia: ‘Usiache kusikia kilio changu cha msaada bali unipatie nafuu.’ Nilipokuita ulinijia karibu ukaniambia, ‘Usiogope!’ “Umenitetea katika kisa changu ee Mwenyezi-Mungu, umeyakomboa maisha yangu. Umeuona uovu niliotendewa ee Mwenyezi-Mungu, uniamulie kwa wema kisa changu. Umeuona uovu wa maadui zangu, na mipango yao yote ya hila dhidi yangu. “Umesikia matukano yao ee Mwenyezi-Mungu, na mipango yao yote ya hila dhidi yangu. Maneno na mawazo ya maadui zangu siku nzima ni juu ya kuniangamiza mimi. Wakati wote, wamekaa au wanakwenda, mimi ndiye wanayemzomea. Uwalipize, ee Mwenyezi-Mungu kadiri ya hayo matendo yao, kadiri ya mambo waliyotenda wenyewe. Uipumbaze mioyo yao, na laana yako iwashukie. Uwafuatie kwa hasira, uwaangamize, uwafanye watoweke ulimwenguni.” Jinsi gani dhahabu yetu ilivyochujuka, dhahabu safi kabisa ilivyobadilika! Mawe ya thamani yametawanywa yamesambaa barabarani kote. Watoto wa Siyoni waliosifika sana, waliothaminiwa kama dhahabu safi, jinsi gani sasa wamekuwa kama vyombo vya udongo, kazi ya mikono ya mfinyanzi! Hata mbwamwitu huwa na hisia za mama na kuwanyonyesha watoto wao; lakini watu wangu wamekuwa wakatili, hufanya kama mbuni nyikani. Midomo ya watoto wachanga imekauka kwa kiu, watoto wanaomba chakula lakini hakuna anayewapa. Watu waliojilisha vyakula vinono sasa wanakufa njaa barabarani. Waliolelewa na kuvikwa kifalme sasa wanafukua kwa mikono kwenye majaa. Watu wangu wamepata adhabu kubwa kuliko watu wa mji wa Sodoma mji ambao uliteketezwa ghafla bila kuwa na muda wa kunyosha mkono. Vijana wa Siyoni walikuwa safi kuliko theluji, walikuwa weupe kuliko maziwa. Miili yao ilikuwa myekundu kama matumbawe, uzuri wa viwiliwili vyao kama johari ya rangi ya samawati. Sasa sura zao ni nyeusi kuliko makaa, wanapita barabarani bila kujulikana; ngozi yao imegandamana na mifupa yao imekauka, imekuwa kama kuni. Afadhali waliouawa kwa upanga kuliko waliokufa kwa njaa, ambao walikufa polepole kwa kukosa chakula. Kina mama ambao huwa na huruma kuu waliwapika watoto wao wenyewe, wakawafanya kuwa chakula chao wakati watu wangu walipoangamizwa. Mwenyezi-Mungu alionesha uzito wa ghadhabu yake, aliimimina hasira yake kali; aliwasha moto huko mjini Siyoni ambao uliteketeza misingi yake. Wafalme duniani hawakuamini wala wakazi wowote wa ulimwenguni, kwamba mvamizi au adui angeweza kuingia malango ya Yerusalemu. Hayo yalisababishwa na dhambi za manabii wake, yalitukia kwa sababu ya uovu wa makuhani wake ambao walimwaga damu ya waadilifu mjini kwake. Walitangatanga barabarani kama vipofu, walikuwa wamekuwa najisi kwa damu, hata asiwepo mtu yeyote wa kuwagusa. Watu waliwapigia kelele wakisema: “Tokeni, nendeni zenu enyi mlio najisi! Tokeni, tokeni, msiguse chochote.” Hivyo wakawa wakimbizi na kutangatanga; watu wa mataifa walitamka: “Hawa hawatakaribishwa kukaa kwetu!” Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwatawanya, wala hatawajali tena. Makuhani hawatapata tena heshima, wazee hawatapendelewa tena. Tulichoka kukaa macho kungojea msaada; tulikesha na kungojea kwa hamu taifa ambalo halikuweza kutuokoa. Watu walifuatilia hatua zetu, tukashindwa kupita katika barabara zetu. Siku zetu zikawa zimetimia; mwisho wetu ukawa umefika. Waliotufuatia walikuwa wepesi kuliko tai, walitukimbiza milimani, walituvizia huko nyikani. Walimnasa yule ambaye maisha yetu yalimtegemea, yule mfalme aliyewekwa wakfu wa Mwenyezi-Mungu, yule ambaye tulisema: “Chini ya ulinzi wake tutaishi miongoni mwa mataifa.” Wakazi wa Edomu, mwaweza kushangilia kwa sasa, mwaweza kwa sasa kufurahi enyi wakazi wa Uzi; lakini kikombe hiki cha adhabu kitawajia pia, nanyi pia mtakinywa na kulewa, hata mtayavua mavazi yenu! Adhabu ya uovu wako ewe Siyoni imekamilika; Mwenyezi-Mungu hatawaacha zaidi uhamishoni. Lakini nyinyi Waedomu atawaadhibu kwa uovu wenu, atazifichua dhambi zenu. Ukumbuke ee Mwenyezi-Mungu, mambo yaliyotupata! Utuangalie, uone jinsi tulivyoaibishwa! Nchi yetu imekabidhiwa wageni, nyumba zetu watu wengine. Tumekuwa yatima, bila baba, mama zetu wameachwa kama wajane. Maji yetu tunayapata kwa fedha, kuni zetu kwa kuzinunua. Tunalazimishwa kufanya kazi kama punda, tumechoka lakini haturuhusiwi kupumzika. Wamisri na Waashuru tumewanyoshea mikono, ili tupate chakula cha kutosha. Wazee wetu walitenda dhambi na hawapo tena; nasi tunateseka kwa sababu ya makosa yao. Watumwa ndio wanaotutawala, wala hakuna wa kutuokoa mikononi mwao. Chakula chetu twapata kwa kuhatarisha maisha yetu, maana wauaji wanazurura huko mashambani. Ngozi zetu zawaka moto kama tanuri kwa sababu ya njaa inayotuchoma. Wanawake wetu wanashikwa kwa nguvu mjini Siyoni, binti zetu katika vijiji vya Yuda. Wakuu wetu wametungikwa kwa mikono yao; wazee wetu hawapewi heshima yoyote. Vijana wanalazimishwa kusaga nafaka kwa mawe, wavulana wanayumbayumba kwa mizigo ya kuni. Wazee wameacha kutoa mashauri yao, vijana wameacha kuimba. Furaha ya mioyo yetu imetoweka, ngoma zetu zimegeuzwa kuwa ombolezo. Fahari tuliyojivunia imetokomea. Ole wetu kwa kuwa tumetenda dhambi! Kwa ajili hiyo tumeugua moyoni, kwa mambo hayo macho yetu yamefifia. Maana mlima Siyoni umeachwa tupu, mbweha wanazurura humo. Lakini wewe Mwenyezi-Mungu watawala milele, utawala wako wadumu vizazi vyote. Mbona umetuacha muda mrefu hivyo? Mbona umetutupa siku nyingi hivyo? Uturekebishe ee Mwenyezi-Mungu, nasi tukurudie, uturudishie fahari yetu kama zamani. Au, je, umetukataa kabisa? Je, umetukasirikia mno? Mnamo siku ya tano ya mwezi wa nne, mwaka wa thelathini, nilikuwa Babuloni kwenye mto Kebari miongoni mwa wale watu waliopelekwa uhamishoni. Basi, mbingu zilifunguka, nikaona maono ya Mungu. Katika siku hiyo ya tano ya mwezi (ulikuwa mwaka wa tano baada ya mfalme Yehoyakini kupelekwa uhamishoni Babuloni), Mwenyezi-Mungu aliongea nami kuhani Ezekieli mwana wa Buzi, nilipokuwa Kaldayo karibu na mto Kebari, naye Mwenyezi-Mungu akaniwekea mkono wake. Nilipotazama niliona upepo wa dhoruba unavuma kutoka kaskazini: Kulikuwa na wingu kubwa lililozungukwa na mngao, na moto ulichomoza humo mfululizo na katikati ya huo moto kulikuwa na kitu kinametameta kama shaba. Kutoka humo nilibainisha viumbe hai wanne, ambao walionekana hivi: Walikuwa na umbo la binadamu. Kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyoka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Walikuwa na mikono ya binadamu chini ya mabawa yao katika pande zao nne. Ncha za mabawa yao ziligusana kila bawa na bawa lingine. Waliposogea, upande wowote ule, walikwenda mbele moja kwa moja bila kugeuza miili yao. Kuhusu nyuso zao nne kila mmoja wao alikuwa na uso wa binadamu upande wa mbele, uso wa simba upande wa kulia, uso wa ng'ombe upande wa kushoto, na uso wa tai upande wa nyuma. Mabawa mawili ya kila mmoja yalikuwa yamekunjuliwa juu na kugusana na kwa mabawa yale mengine mawili walifunika miili yao. Popote roho ilipotaka kwenda, walikwenda; kila mmoja wao alikwenda mbele moja kwa moja bila kuugeuza mwili wake. Katikati ya hao viumbe hai kulikuwa na kitu kilichoonekana kama makaa yanayowaka moto, kama miali ya moto iliyomulika huku na huko kati ya hao viumbe. Moto huo ulikuwa mwangavu na umeme ulichomoza humo. Viumbe hao pia walikwenda huku na huko kama pigo la umeme. Nilipokuwa nawatazama hao viumbe hai niliona chini karibu na kila kiumbe kulikuwa na gurudumu. Magurudumu hayo yalionekana kuwa ya namna moja, yanametameta kama jiwe la zabarajadi na muundo wao ulikuwa kama gurudumu ndani ya gurudumu lingine. Yaliposogea yalikwenda upande wowote wa pande nne za dira ya dunia bila kugeuka. Mizingo ya hayo magurudumu ilikuwa mirefu kutisha na mizingo ya magurudumu hayo ilikuwa imejaa macho pande zote. Hao viumbe hai walipokwenda, magurudumu nayo yalikwenda kandokando yao; na viumbe hao walipoinuka juu kutoka ardhini, magurudumu hayo yaliinuka. Popote roho ilipokwenda walikwenda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja nao; maana roho ya hao viumbe hai ilikuwa katika magurudumu hayo. Viumbe hao walipokwenda, magurudumu nayo yalikwenda; waliposimama, nayo yalisimama; walipoinuka juu kutoka ardhini, magurudumu nayo yaliinuka pamoja nao. Maana roho ya hao viumbe hai ilikuwa katika magurudumu hayo. Juu ya vichwa vya hao viumbe hai kulikuwa na kitu mfano wa anga, kinangaa kama kioo. Chini ya kitu hicho walisimama hao viumbe hai; mabawa mawili ya hao viumbe yalikuwa yamekunjuliwa kuelekeana, na kwa mabawa mengine mawili walifunika miili yao. Walipokuwa wanakwenda, nilisikia sauti ya mabawa yao; sauti ya mvumo huo ilikuwa kama ile ya maji mengi, kama sauti ya ngurumo kutoka kwa Mungu wa majeshi, na kama kelele ya jeshi kubwa. Waliposimama, walikunja mabawa yao. Nilisikia sauti kutoka juu ya kitu kile kama anga kilichokuwa juu ya vichwa vyao. Juu ya kitu hicho niliona kitu kama kiti cha enzi cha johari ya rangi ya samawati. Juu yake aliketi mmoja anayefanana na binadamu. Sehemu ya juu ya mwili wake ilingaa kama shaba, kama moto uliozunguka pande zote; sehemu ya chini ya mwili wake ilikuwa kama moto nayo ilizungukwa na mngao ulioonekana kama upinde wakati wa mvua. Ndivyo ulivyoonekana mfano wa utukufu wa Mwenyezi-Mungu. Nilipouona, nilianguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea. Naye akaniambia, “Wewe mtu! Simama wima. Nataka kuongea nawe.” Alipokuwa akiongea nami, roho ya Mungu ikaniingia na kunisimamisha wima. Ndipo nikamsikia akiniambia, “Wewe mtu nakutuma kwa Waisraeli, taifa la waasi ambao wameniasi. Wameendelea kunikosea mimi hadi leo kama walivyokuwa wazee wao. Watu hao ni wafidhuli na wajeuri. Nakutuma kwao, nawe utawaambia kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi. Wakisikia au wasiposikia, maana wao ni watu waasi, walau watatambua kwamba nabii amekuwapo miongoni mwao. Lakini, ewe mtu usiwaogope hao wala maneno yao. Hata kama mbigili na miiba vinakuzunguka, au unaketi juu ya nge, usiogope maneno yao wala usitishwe na nyuso zao, kwani hao ni watu waasi. Wewe utawaambia maneno yangu, hata kama watasikia au hawatasikia, maana wao ni watu waasi. “Lakini ewe mtu, sikiliza ninayokuambia, wala usiwe mwasi kama watu hao. Fumbua kinywa chako, ule ninachokupa.” Nilipotazama, niliona nimenyoshewa mkono, na kumbe ulikuwa na kitabu kilichoandikwa. Basi akakifungua mbele yangu, nacho kilikuwa kimeandikwa mbele na nyuma maneno ya maombolezo, vilio na laana. Akaniambia, “Wewe mtu, kula unachopewa; kula kitabu hiki kisha uende ukawaeleze Waisraeli.” Kwa hiyo nilifumbua kinywa changu, naye akanilisha hicho kitabu. Halafu akaniambia, “Wewe mtu, kula kitabu hiki ninachokupa, ujaze tumbo lako.” Basi, nilikula kitabu hicho, nacho kikawa kitamu mdomoni kama asali. Kisha akaniambia, “Wewe mtu, waendee Waisraeli, ukawaambie maneno yangu. Sikutumi kwa taifa lenye lugha ngeni na ngumu, bali kwa Waisraeli. Sikutumi kwa mataifa mengi yenye lugha ngeni na ngumu ambayo huifahamu. Kwani ningelikutuma kwa watu kama hao, hakika wao wangekusikiliza. Lakini Waisraeli hawatakusikiliza, kwani hawana nia ya kunisikiliza mimi. Watu wote wa Israeli ni wenye kichwa kigumu na moyo mkaidi. Nimekufanya uwe mgumu dhidi yao, na kichwa chako kitakuwa kigumu dhidi ya vichwa vyao vigumu. Kama almasi ilivyo ngumu kuliko jiwe gumu, ndivyo nilivyokufanya uwe kichwa kigumu. Usiwaogope wala usitishwe na nyuso zao, kwani hao ni watu waasi.” Tena aliniambia, “Wewe mtu, maneno yote nitakayokuambia yatie moyoni mwako, na uyasikilize kwa makini. Kisha nenda kwa watu wako waliopelekwa uhamishoni, ukawaambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi. Waambie hata kama watakusikiliza au watakataa kukusikiliza.” Kisha roho ya Mungu ikaninyanyua, nami nikasikia nyuma yangu sauti kama ya tetemeko kubwa. “Na usifiwe utukufu wa Mwenyezi-Mungu mbinguni.” Pia nilisikia sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yalipokuwa yanagusana, pamoja na sauti ya mgongano wa yale magurudumu kandokando yao. Basi, roho ya Mungu ikaninyanyua juu na kunipeleka mbali. Nikaenda nikiwa na uchungu na ukali rohoni mwangu, nao mkono wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa na nguvu juu yangu. Nikawafikia wale watu waliokuwa uhamishoni, waliokuwa wakikaa karibu na mto Kebari huko Tel-abibu. Nikakaa nao kwa muda wa siku saba nikiwa nimepigwa bumbuazi. Baada ya siku saba, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu nimekuweka kuwa mlinzi wa Waisraeli. Kila utakaposikia neno kutoka kwangu utawaonya watu kwa niaba yangu. Nikimwambia mtu mwovu kwamba hakika atakufa, nawe humwonyi au kumwambia aache njia yake potovu ili kuyaokoa maisha yake, basi, mtu huyo mwovu atakufa kwa uovu wake; lakini damu yake nitakudai wewe. Lakini, ukimwonya mtu huyo mwovu naye hauachi uovu wake au njia yake potovu, mtu huyo atakufa kwa uovu wake, lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako. Tena, kama mtu mwadilifu anauacha uadilifu wake na kutenda uovu, nami nikamwekea kikwazo, mtu huyo atakufa. Kwa vile hukumwonya, atakufa kwa sababu ya dhambi yake, nayo matendo yake ya uadilifu hayatakumbukwa. Lakini damu yake nitakudai wewe. Lakini, ukimwonya mtu mwadilifu asitende dhambi, naye akaacha kutenda dhambi, hakika mtu huyo ataishi, kwa kuwa amepokea maonyo yako, nawe utakuwa umeyaokoa maisha yako.” Nguvu ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa juu yangu; naye akaniambia, “Inuka uende mpaka sehemu tambarare nami nitaongea nawe huko.” Basi, nikainuka na kwenda sehemu tambarare. Lo! Nikiwa huko nikauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukiwa umesimama huko kama utukufu ule niliokuwa nimeuona karibu na mto Kebari; nami nikaanguka kifudifudi. Lakini roho iliniingia na kunisimamisha wima. Kisha Mungu akaongea nami, akaniambia, “Nenda ukajifungie nyumbani mwako. Ewe mtu, utafungwa kwa kamba ili usiweze kutoka na kuwaendea watu. Nitaufanya ulimi wako uwe mzito nawe utakuwa bubu ili usiweze kuwakemea kwa sababu ni waasi. Lakini kila nitakapoongea nawe nitakifungua kinywa chako, nawe utawaambia kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi, atakayekusikiliza, na akusikilize; atakayekataa kukusikiliza na akatae; maana hao ni watu waasi. “Wewe mtu, chukua tofali, uliweke mbele yako; kisha chora juu yake ramani ya mji wa Yerusalemu. Onesha kuwa umezingirwa. Chora ngome dhidi yake na maboma kandokando yake, makambi ya askari kandokando yake, na magogo ya kuubomolea. Kisha, chukua bamba la chuma ulisimamishe liwe kama ukuta wa chuma kati yako na mji. Kisha uelekee mji huo unaozingirwa, uoneshe kana kwamba unazingirwa. Fanya alama ya kuuzingira. Hii itakuwa ishara kwa taifa la Israeli. “Kisha, nenda ukalale kwa upande wako wa kushoto. Muda wote utakapokaa katika hali hiyo utabeba uovu wa Waisraeli kama mzigo mzito. Nimekupangia muda wa siku 390 muda ambao ni sawa na miaka ya adhabu yao. Siku moja ni sawa na mwaka mmoja. Utabeba adhabu ya Waisraeli. Utakapotimiza siku hizo, utalala kwa upande wa kulia, na hapo utabeba adhabu ya watu wa Yuda kwa muda wa siku arubaini; nimekupangia siku moja kuwa sawa na mwaka mmoja. “Kisha, utauelekea mji wa Yerusalemu uliozingirwa na kuunyoshea mkono mtupu na kutabiri dhidi yake. Nitakufunga kamba ili usiweze kugeuka toka upande mmoja hadi upande mwingine, mpaka hapo kuzingirwa kwa Yerusalemu kutakapomalizika. “Chukua ngano, shayiri, maharagwe, choroko, mtama na mawele, uvitie vyote katika chombo kimoja, ujitengenezee mkate. Mkate huo ndio utakaokuwa chakula chako wakati unapolala kwa upande mmoja, siku zote 390. Chakula utakachokula lazima kipimwe, nacho kitakuwa gramu 230 kwa siku; nawe utakula mara moja tu kwa siku. Maji nayo utakunywa kwa kipimo: Vikombe viwili, mara moja kwa siku. Utachukua mavi ya mtu, uwashe moto, uoke mkate, na kuula mbele ya watu.” Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Hivyo ndivyo Waisraeli watakavyokula mkate wao unajisi wakiwa kati ya mataifa ninakowapeleka.” Ndipo nikamwambia, “Ee, Bwana Mwenyezi-Mungu, kamwe sijajitia najisi kwa kula kilichokufa chenyewe au kilichouawa na mnyama wa porini, wala sijapata kuonja nyama ya mnyama najisi tangu ujana wangu.” Kisha akaniambia, “Basi, nakuruhusu utumie mavi ya ng'ombe badala ya mavi ya mtu ili kuokea mkate wako.” Tena akaniambia, “Wewe mtu, mimi nitaharibu akiba ya chakula mjini Yerusalemu; wakazi wake watakula chakula watakachopimiwa kwa hofu. Watakunywa maji watakayopimiwa kwa kufadhaika. Nitafanya hivyo ili wakose chakula na maji, na kila mmoja atamwangalia mwenzake kwa kufadhaika; nao watadhoofika kwa adhabu yao.” Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Wewe mtu, jipatie upanga mkali, uutumie kama wembe wa kinyozi. Upitishe kichwani pako na kidevuni ili kunyoa nywele zako pamoja na ndevu zako. Kisha twaa mizani, uzipime nywele zako ili kuzigawanya. Baada ya kuzingirwa kwa mji wa Yerusalemu kumalizika, utaichoma theluthi ya nywele zako ndani ya mji. Theluthi nyingine utaipigapiga kwa upanga ukiuzunguka mji. Theluthi ya mwisho utaitawanya kwa upepo, nami nitauchomoa upanga wangu ili kuifuatilia. Sehemu ndogo tu ya nywele zako utaichukua na kuifunga kwenye mkunjo wa joho lako. Lakini chukua pia nywele kidogo uzitupe motoni na kuziteketeza. Moto utatokea humo na kuwaunguza watu wote wa Israeli. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ndivyo itakavyokuwa kuhusu mji wa Yerusalemu. Mimi niliuweka kuwa katikati ya mataifa, umezungukwa na nchi za kigeni pande zote. Lakini wakazi wake wameyaasi maagizo na kanuni zangu, wakawa wabaya kuliko mataifa na nchi zinazowazunguka. Naam, wameyakataa maagizo yangu na kuacha kuzifuata kanuni zangu. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa kuwa nyinyi ni wakaidi kuliko mataifa yanayowazunguka, kwa kuwa hamkuishi kulingana na kanuni zangu, wala hamkuyashika maagizo yangu, ila mmetenda kulingana na maagizo ya mataifa yanayowazunguka, basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitazitekeleza hukumu zangu dhidi yenu mbele ya mataifa. Kutokana na machukizo yenu yote nitawaadhibu kwa adhabu ambayo sijapata kuwapeni na ambayo sitairudia tena. Hukohuko mjini wazazi watawala watoto wao wenyewe na watoto watawala wazazi wao. Nitatekeleza hukumu zangu dhidi yenu na watakaobaki hai nitawatawanya pande zote. Kwa sababu hiyo, kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, kwa vile mmeitia unajisi maskani yangu kwa machukizo yenu, mimi nitawakatilia mbali bila huruma na bila kumwacha mtu yeyote. Theluthi moja ya watu wako, ee Yerusalemu, itakufa kwa maradhi mabaya na kwa njaa; theluthi nyingine itakufa vitani na theluthi inayobaki nitaitawanya pande zote za dunia na kuwafuatilia kwa upanga. “Ndivyo hasira yangu itakavyoishia, nami nitakuwa nimetuliza ghadhabu yangu na kuridhika moyoni. Hapo ndipo watakapojua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nimewaadhibu kwa kukosa uaminifu kwangu. Tena, wewe mji wa Yerusalemu nitakufanya kuwa ukiwa na kitu cha dhihaka miongoni mwa mataifa yanayokuzunguka na mbele ya watu wote wapitao karibu nawe. Utakuwa kitu cha dharau na aibu, mfano wa kitu cha kuchukiza kwa makabila yanayokuzunguka, wakati nitakapotekeleza hukumu zangu dhidi yako kwa hasira na ghadhabu yangu kali. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wakati huo nitaiachilia mishale yangu mikali ya njaa iwachome na kuangamiza wakazi wako. Nitawafanya wafe njaa kwa kuiharibu akiba yao ya chakula. Nitakupelekea njaa na wanyama wakali ambao watakupokonya watoto wako; maradhi mabaya, mauaji, na vita vitakuja kukuangamiza. Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, igeukie milima ya Israeli, utangaze ujumbe huu wangu dhidi ya wakazi wake na kusema: Sikilizeni neno la Bwana Mwenyezi-Mungu enyi wakazi wa milima ya Israeli: Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambieni nyinyi wakazi wa milimani na vilimani, wa magengeni na mabondeni kwamba mimi mwenyewe nitaleta upanga na kuharibu sehemu zenu zote zilizoinuka za ibada. Madhabahu zenu zitaharibiwa na mahali penu pa kufukizia ubani patavunjwavunjwa. Wale watakaouawa nitawatupa mbele ya sanamu zenu za miungu. Maiti za Waisraeli nitazilaza mbele ya sanamu zao za miungu, na mifupa yenu nitaitawanya kandokando ya madhabahu zenu. Kokote mnakoishi, miji yenu itakuwa ukiwa na sehemu za mwinuko za ibada zenu zitabomolewa, madhabahu zenu ziwe uharibifu na maangamizi, sanamu zenu za miungu zivunjwe na kuharibiwa. Mahali penu pa kufukizia ubani patabomolewa na chochote mlichofanya kitatokomezwa. Wale watakaouawa wataanguka kati yenu, nanyi mtatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Hata hivyo, nitawaacha wengine wabaki hai; baadhi yenu watanusurika kuuawa nao watatawanyika katika nchi mbalimbali. Ndipo watakaponikumbuka mimi miongoni mwa hao watu wa mataifa ambamo watatawanyika. Watakumbuka jinsi nilivyowapiga kwa sababu mioyo yao isiyo na uaminifu ilinigeuka na kwa vile waliacha kunitazamia mimi wakazitazamia sanamu za miungu. Kwa hiyo watajichukia wao wenyewe kwa sababu ya maovu na machukizo yao yote waliyoyatenda. Hapo ndipo watakapojifunza kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu; sikuwatisha bure ya kwamba nitawaletea maovu hayo yote.” Bwana Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Piga makofi, piga kishindo kwa mguu na kusema: Ole wenu Waisraeli kwa sababu ya machukizo yenu yote, kwani mtakufa kwa upanga, njaa na kwa maradhi mabaya. Aliye mbali sana atakufa kwa maradhi mabaya. Aliye karibu atauawa kwa upanga. Atakayekuwa amebaki na kunusurika hayo mawili atakufa kwa njaa. Ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu dhidi yao. Maiti zao zitatapakaa kati ya sanamu zao za miungu na madhabahu zao, juu ya kila mlima, chini ya kila mti mbichi, chini ya kila mwaloni wenye majani na kila mahali walipotolea tambiko zao za harufu nzuri ya kuzipendeza sanamu zao za miungu. Hapo ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nitaunyosha mkono wangu dhidi yao, na kuiharibu nchi yao. Tangu huko jangwani kusini mpaka mjini Ribla kaskazini, nitaifanya nchi yao kuwa mahame kabisa wasipate mahali pa kuishi. Hapo ndipo wote watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, waambie wakazi wa nchi ya Israeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Sasa ni mwisho! Mwisho umeifikia nchi yote kutoka pande zote nne! Sasa mwisho umewafikia; sasa mtausikia ukali wa hasira yangu juu yenu. Nitawahukumu kadiri ya mwenendo wenu. Nitawaadhibu kwa machukizo yenu yote. Sitawaachia wala sitawahurumia; nitawaadhibu kulingana na mienendo yenu, maadamu machukizo bado yapo kati yenu. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Ninachosema mimi Bwana Mwenyezi-Mungu ni hiki: Mtapatwa na maafa mfululizo! Mwisho umekuja! Naam, mwisho umefika! Umewafikia nyinyi! Enyi wakazi wa nchi hii, maangamizi yenu yamewajia! Wakati umekuja; naam, siku imekaribia. Hiyo ni siku ya msukosuko na siyo ya sauti za shangwe mlimani. Sasa mtausikia uzito wa hasira yangu juu yenu. Nitawahukumu kulingana na mwenendo wenu; nitawaadhibu kadiri ya machukizo yenu. Sitawaachilia wala sitawaonea huruma. Nitawaadhibu kulingana na mienendo yenu maadamu machukizo yapo bado miongoni mwenu. Ndipo mtakapotambua kuwa ni mimi Mwenyezi-Mungu ninayewaangamiza. “Tazameni, siku ile inakuja! Maangamizi yenu yamekuja. Ukatili uko kila mahali na kiburi kimechanua. Ukatili unaendelea kuwa mbaya zaidi. Hakuna hata mmoja wenu atakayebaki, wala vitu mlivyojirundikia kwa wingi au utajiri wenu; hatakuwako mtu mwenye heshima miongoni mwenu. Wakati umewadia, naam, ile siku imekaribia. Mnunuzi asifurahi wala mwuzaji asiomboleze; kwa sababu ghadhabu yangu itaukumba umati wote. Wauzaji hawataweza kurudia mali yao waliyouza hata kama wakibaki hai. Kwani maono haya yahusu umati wote na hayatabatilishwa. Kutokana na uovu huo, hakuna mtu atakayesalimisha maisha yake. Tarumbeta imepigwa na kuwafanya wote wawe tayari. Lakini hakuna anayekwenda vitani, kwani ghadhabu yangu iko juu ya umati wote. Nje kuna kifo kwa upanga na ndani ya mji kuna maradhi mabaya na njaa. Walioko shambani watakufa kwa upanga; walio mjini njaa na maradhi mabaya yatawaangamiza. Wakiwapo watu watakaosalimika watakimbilia milimani kama hua waliotishwa bondeni. Kila mmoja wao ataomboleza kwa dhambi zake. Kila mtu, mikono yake itakuwa dhaifu na magoti yake yatakuwa maji. Watavaa mavazi ya gunia, hofu itawashika, nao watakuwa na aibu, vichwa vyao vyote vitanyolewa. Watatupa fedha yao barabarani na dhahabu yao itakuwa kama kitu najisi. Fedha na dhahabu zao hazitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu; wala hawataweza kushiba au kuyajaza matumbo yao fedha na dhahabu waliyojirundikia; kwani mali hiyo ndiyo chanzo cha dhambi yao. Kwa kuwa walijifanyia utukufu usio na maana kwa njia ya vikuku, wakajifanyia sanamu za miungu zinazochukiza pamoja na vitu vyao vya aibu; vyote hivyo nitavifanya kuwa najisi kwao. Utajiri wao nitautia mikononi mwa mataifa mengine, watu waovu wa dunia watauteka na kuutia najisi. Uso wangu nitaugeuzia mbali nao ili walitie najisi hekalu langu. Wanyanganyi wataingia humo ndani na kulitia najisi. Tengeneza mnyororo. Kwa kuwa nchi imejaa makosa ya jinai ya umwagaji damu na mji umejaa dhuluma kupindukia, nitayaleta mataifa mabaya sana nao watazimiliki nyumba zao. Kiburi chao nitakikomesha, na mahali pao pa ibada patatiwa unajisi. Uchungu mkali utakapowajia, watatafuta amani, lakini haitapatikana. Watapata maafa mfululizo; nazo habari mbaya zitafuatana. Watamwomba nabii maono. Makuhani hawatakuwa na sheria yoyote; na wazee watakosa shauri la kuwapatia. Mfalme ataomboleza, mkuu atakata tamaa na watu watatetemeka kwa hofu. Nitawatenda kadiri ya mienendo yao, nitawahukumu kama nilivyowahukumu wengine. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Katika mwaka wa sita, siku ya tano ya mwezi wa sita, nilikuwa nyumbani kwangu pamoja na wazee wa Yuda. Basi, ghafla nikakumbwa na nguvu ya Mwenyezi-Mungu. Nilipotazama, nikaona maono: Kitu kilichofanana na binadamu. Sehemu yake ya chini, iliyoonekana kama ndio kiuno chake, ilikuwa kama moto. Toka kiuno chake kwenda juu alikuwa na mngao kama wa shaba ingaayo. Basi, akanyosha kitu kama mkono, akanishika kwa nywele zangu. Roho ya Mungu ikaninyanyua kati ya ardhi na mbingu, ikanipeleka mpaka Yerusalemu nikiwa katika maono hayo ya Mungu. Nikafika kwenye kiingilio cha lango la ukumbi wa ndani linaloelekea upande wa kaskazini, mahali palipowekwa sanamu iliyomchukiza Mungu. Utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo; nao ulikuwa kama utukufu ule niliouona katika maono kule bondeni. Kisha Mungu akaniambia, “Wewe mtu, tazama upande wa kaskazini.” Nami nikatazama upande wa kaskazini, na huko upande wa kaskazini wa lango la madhabahu, niliona ile sanamu iliyomchukiza Mungu. Basi, Mungu akaniambia, “Wewe mtu, je, waona mambo wanayofanya, machukizo makubwa wanayofanya Waisraeli ili wapate kunifukuza kutoka maskani yangu? Tena utaona machukizo mengine makubwa zaidi.” Kisha akanipeleka mpaka lango la ua. Nilipoangalia nikaona tundu ukutani. Naye akaniambia, “Wewe mtu, toboa ukuta huu.” Nami, nikatoboa, nikaona kulikuwa na mlango. Naye akaniambia, “Ingia ndani ukaangalie machukizo mabaya wanayofanya humo.” Basi, nikaingia, nikaona sanamu za wadudu na za wanyama wa kila aina ya kuchukiza na vinyago vyote vya miungu ya Waisraeli, vimechorwa kuuzunguka ukuta. Na mbele ya sanamu hizo walisimama wazee sabini wa watu wa Israeli pamoja na Yaazania mwana wa Shafani. Kila mmoja alikuwa na chetezo mkononi, na moshi wa ubani ulipanda juu. Kisha Mungu akaniambia, “Wewe mtu, umeona wanayotenda wazee wa Waisraeli gizani, kila mtu katika chumba chake cha sanamu. Wanadai ati Mwenyezi-Mungu hatuoni. Mwenyezi-Mungu ameiacha nchi.” Tena akaniambia, “Bado utaona machukizo makubwa zaidi wanayotenda.” Kisha akanichukua mpaka lango la kaskazini la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko kulikuwa na wanawake wameketi wakimwombolezea Tamuzi. Mungu akaniambia: “Wewe mtu, umeyaona hayo? Bado utaona machukizo mengine makubwa kuliko hayo.” Kisha akanipeleka mpaka ua wa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko mlangoni mwa hekalu, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwapo wanaume wapatao ishirini na watano, wakilipa kisogo hekalu, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki. Walikuwa wanaabudu jua wakielekea upande wa mashariki. Mungu akaniambia, “Wewe mtu, je umeyaona mambo hayo? Hata hivyo, watu wa Yuda wanaona machukizo hayo kuwa ni kidogo. Wanaijaza nchi dhuluma na kuzidi kunikasirisha. Angalia jinsi wamekaa hapo, wananiudhi kupita kiasi. Kwa sababu ya mambo hayo watasikia uzito wa ghadhabu yangu. Sitamwacha hata mmoja aponyoke wala sitamwonea huruma mtu yeyote. Hata wakinililia kwa sauti kubwa mimi sitawasikiliza.” Kisha nikamsikia Mwenyezi-Mungu akisema kwa sauti kubwa: “Njoni karibu nyinyi mtakaouadhibu mji huu. Njoni na silaha zenu za kuangamiza.” Watu sita wakaja kutoka upande wa lango la juu linaloelekea kaskazini, kila mmoja na silaha yake ya kuangamiza mkononi mwake. Pamoja nao, alikuwapo mtu mmoja ambaye alikuwa amevaa mavazi ya kitani, naye ana kidau cha wino. Wakaingia ndani ya hekalu, wakasimama pembeni mwa madhabahu ya shaba. Kisha utukufu wa Mungu wa Israeli uliondoka pale juu ya kiumbe chenye mabawa na kupanda juu mpaka kizingiti cha nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa mavazi ya kitani, mwenye kidau cha wino, akamwambia, “Pita katikati ya mji wa Yerusalemu, ukatie alama kwenye vipaji vya nyuso za watu wanaohuzunika na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayotendeka katika mji huu.” Kisha akawaambia wale wengine mimi nikiwa nasikia, “Piteni mjini mkimfuata, mkaue watu; msimwachie yeyote wala msiwe na huruma. Waueni wazee papo hapo, wavulana kwa wasichana, watoto na wanawake; lakini kila mmoja mwenye alama, msimguse. Anzeni katika maskani yangu.” Basi, wakaanza na wazee waliokuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Akawaambia, “Tieni unajisi nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa kuzijaza nyua zake maiti. Songeni mbele.” Basi, wakaenda, wakawaua watu mjini. Wakati walipokuwa wakiwaua, mimi niliachwa peke yangu, nikaanguka kifudifudi, nikalia, “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, je, utaangamiza watu wote wa Israeli waliobaki, ukitimiza ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?” Naye akaniambia, “Uovu wa watu wa Israeli na watu wa Yuda ni mkubwa sana. Nchi imejaa umwagaji damu na mjini hakuna haki, kwani wanasema: ‘Mwenyezi-Mungu ameiacha nchi; Mwenyezi-Mungu haoni.’ Kwa upande wangu, sitawaachia wala kuwahurumia; nitawatenda kadiri ya matendo yao.” Kisha mtu yule aliyevaa mavazi ya kitani, mwenye kidau cha wino, akarudi na kutoa taarifa: “Nimefanya kama ulivyoniamuru.” Kisha nikaona kwamba katika lile anga juu ya vichwa vya viumbe wenye mabawa kulikuwa na kitu kinachofanana na johari ya rangi ya samawati, umbo lake kama kiti cha enzi. Mungu akamwambia yule mtu aliyevaa mavazi ya kitani, “Nenda katikati ya magurudumu yaliyo chini ya viumbe wenye mabawa, ukaijaze mikono yako makaa ya moto ulioko katikati yao na kuyatawanya juu ya mji.” Nikamwona akienda. Wale viumbe wenye mabawa walikuwa wamesimama upande wa kusini wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu yule mtu alipoingia ndani; wingu likaujaza ua wa ndani. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukapaa juu kutoka kwa wale viumbe wenye mabawa ukaenda kwenye kizingiti cha nyumba hiyo, na lile wingu likaijaza nyumba, na ua ukajaa mngao wa utukufu wa Mwenyezi-Mungu. Mlio wa viumbe wenye mabawa uliweza kusikika hata kwenye ua wa nje, kama sauti ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi anapoongea. Mwenyezi-Mungu alipomwamuru yule mtu aliyevaa mavazi ya kitani achukue moto toka katikati ya magurudumu yaliyokuwa chini ya viumbe wenye mabawa, yule mtu alikwenda na kusimama pembeni mwa gurudumu mojawapo. Kiumbe mmoja akanyosha mkono wake kuchukua moto uliokuwa katikati ya viumbe wenye mabawa, akatwaa sehemu yake na kuutia mikononi mwa yule mtu aliyevaa mavazi ya kitani; naye alipoupokea, akaenda zake. Viumbe wenye mabawa hao walionekana kuwa kitu kama mkono wa binadamu chini ya mabawa yao. Niliangalia, nikaona kulikuwa na magurudumu manne, gurudumu moja pembeni mwa kila kiumbe chenye mabawa. Magurudumu hayo yalimetameta kama jiwe la zabarajadi. Yote manne yalionekana kuwa ya namna moja, na kila gurudumu lilionekana kama liko ndani ya gurudumu lingine. Yaliweza kwenda pande zote bila kugeuka; kule lilikoelekea gurudumu la kwanza yote yalifuata. Miili ya hao viumbe, migongo yao, mikono na mabawa yao, pamoja na magurudumu, vyote vilijaa macho pande zote. Niliambiwa kuwa magurudumu yale yanaitwa, “Magurudumu Yanayozunguka.” Kila kiumbe mwenye mabawa alikuwa na nyuso nne: Uso wa kwanza ulikuwa wa fahali, uso wa pili ulikuwa wa mwanadamu, uso wa tatu ulikuwa wa simba na uso wa nne ulikuwa wa tai. Viumbe wenye mabawa wakainuka juu. Hawa ndio wale viumbe hai niliowaona karibu na mto Kebari. Viumbe hao walipokwenda, magurudumu nayo yalikwenda kando yao. Viumbe walipokunjua mabawa yao ili kupaa juu, magurudumu nayo yalikwenda pamoja nao. Waliposimama, magurudumu nayo yalisimama; hao walipopaa juu, magurudumu nayo yalipaa pamoja nao. Roho ya hao viumbe ilikuwa pia katika magurudumu hayo. Kisha utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulitoka kwenye kizingiti cha nyumba, ukaenda na kusimama juu ya wale viumbe. Viumbe wakakunjua mabawa yao, wakapaa juu, mimi nikiwa nawaona na yale magurudumu yalikuwa kando yao. Wakasimama mbele ya lango la mashariki la nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao. Hawa walikuwa wale viumbe hai niliowaona chini ya Mungu wa Israeli karibu na mto Kebari, nami nikatambua kuwa ni viumbe wenye mabawa. Kila mmoja wao alikuwa na nyuso nne na mabawa manne; na chini ya kila bawa kulikuwa na kitu kama mkono wa binadamu. Vilevile nilizitambua nyuso zao: Zilikuwa zilezile nilizokuwa nimeziona kule kwenye mto Kebari. Kila kiumbe alikwenda mbele, moja kwa moja. Roho ya Mungu ikaninyanyua na kunipeleka mpaka lango la mashariki la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko nikawaona watu ishirini na watano wakiwamo Yaazania mwana wa Azuri na Pelatia mwana wa Benaya, ambao ni viongozi wa Waisraeli. Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Wewe mtu, hawa ndio watu watungao uovu na kutoa mashauri mabaya mjini humu. Wanasema, ‘Wakati wa kujenga nyumba bado. Mji ni kama chungu, na sisi ni kama nyama.’ Kwa hiyo, toa unabii dhidi yao! Tabiri ewe mtu!” Kisha roho ya Mwenyezi-Mungu ikanijia, naye akaniambia, “Waambie watu, Mwenyezi-Mungu asema hivi: Naam, hiki ndicho mnachofikiri enyi Waisraeli. Najua mambo mnayofikiria moyoni mwenu. Nyinyi mmewaua watu wengi mjini humu, na kujaza barabara zake na watu waliouawa. “Lakini, mimi, Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Naam, mji huu ni chungu cha kupikia, na wale waliouawa ndio nyama. Nyinyi lazima mtaondolewa mjini. Nyinyi mmeogopa upanga? Basi, mimi nitaleta upanga dhidi yenu! Nitawatoa ndani ya mji na kuwatia mikononi mwa watu wa mataifa mengine, nami nitawahukumu. Mtauawa kwa upanga, nami nitawahukumu mpakani mwa Israeli. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Mji wa Yerusalemu hautakuwa tena chungu chenu wala nyinyi hamtakuwa nyama ndani yake. Mimi nitawahukumu mpakani mwa Israeli. Nanyi mtatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu ambaye sheria zake hamkuzifuata na maagizo yake hamkutekeleza, bali mmetenda kulingana na maagizo ya mataifa yanayowazunguka.” Nilipokuwa natabiri, Pelatia mwana wa Benaya akafariki. Nami nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kubwa, nikisema, “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, je, utawamaliza kabisa Waisraeli waliobaki?” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, ndugu zako na wakazi wa Yerusalemu ambao pia ni ndugu zako wanasema juu yako na juu ya watu wote wa Israeli walioko uhamishoni, ‘Nyinyi mlio uhamishoni mko mbali sana na Mwenyezi-Mungu; maana Mwenyezi-Mungu ametupa sisi nchi hii iwe mali yetu.’ “Lakini, waambie hao walio uhamishoni kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ingawa nimewapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi nyingine, hata hivyo, kwa wakati uliopo mimi nipo pamoja nao huko waliko. “Basi, waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawakusanya toka miongoni mwa watu mnakokaa. Nitawakusanya kutoka nchi ambako mlitawanywa. Nitawarudisha nchini Israeli. Nanyi mtakaporudi nchini mwenu nitaondoa vitu vyote vichafu na machukizo yote. Nitawapeni moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu. Nitauondoa ule moyo mgumu kama jiwe na kuwapa moyo wa utii, ili mpate kufuata kanuni zangu na kuyatii maagizo yangu; nanyi mtakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wenu. Lakini hao ambao moyo wao umeambatana na vitu najisi na machukizo yao, nitawaadhibu kadiri ya mienendo yao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Hapo wale viumbe waliyakunjua mabawa yao na kuanza kuruka pamoja na yale magurudumu yaliyokuwa kando yao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao. Basi, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukapaa juu kutoka katikati ya mji, ukasimama juu ya mlima ulio upande wa mashariki wa mji. Nikiwa katika maono hayo, roho ya Mungu ilininyanyua na kunipeleka mpaka nchi ya Wakaldayo, kwa watu walioko uhamishoni huko. Kisha maono hayo yakatoweka. Hapo nikawaeleza wale waliokuwa uhamishoni mambo yote aliyonionesha Mwenyezi-Mungu. Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu! Wewe unakaa kati ya watu waasi. Wana macho lakini hawaoni; wana masikio lakini hawasikii. Wao ni watu waasi. Basi, ewe mtu, fanya kama vile unakwenda uhamishoni: Ondoka wakiwa wanakuona, ukimbilie mahali pengine. Nenda kama mkimbizi kutoka mahali ulipo mpaka mahali pengine wao wakikuona. Labda wataelewa, ingawa wao ni waasi. Hakikisha wanaona unachofanya. Funga mzigo wako uutoe nje na kuwa tayari kuondoka jioni kama wafanyavyo watu wanaokwenda uhamishoni. Wakiwa wanakuangalia toboa ukuta wa nyumba, upitie hapo na kwenda nje. Wakiwa wanakuona, jitwike mabegani mzigo wako na kuondoka wakati wa giza. Funika uso wako usiweze kuona unakwenda wapi. Ndivyo ninavyokufanya uwe ishara kwa Waisraeli.” Basi, nikafanya kama nilivyoamriwa. Siku hiyo, wakati wa mchana, nikafunga mzigo wangu kama mzigo wa mtu anayekimbia. Jioni nikautoboa ukuta na giza lilipokuwa likiingia, nikatoka, nimejitwika mzigo wangu mabegani, watu wote wakiniona. Kesho yake asubuhi, Mwenyezi-Mungu akaniuliza: “Wewe mtu! Je, hao waasi wa Israeli hawajakuuliza maana ya hicho ulichofanya? Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Kauli hii yangu yahusu mambo yatakayompata mtawala wa Yerusalemu na watu wote wa Israeli wanaoishi humo. Waambie kuwa wewe ni ishara kwao; kama ulivyofanya ndivyo itakavyotendeka kwao: Watakwenda uhamishoni; naam, watachukuliwa mateka. Naye mtawala wao atajitwika mzigo wake mabegani wakati wa usiku, atatoka kupitia ukuta atakaotoboa apate kutoka; atafunika uso wake ili asiione nchi kwa macho yake. Lakini nitatandaza wavu wangu juu yake, naye atanaswa katika mtego wangu. Nitampeleka Babuloni, nchi ya Wakaldayo; naye akiwa huko atakufa bila kuiona hiyo nchi. Wafuasi wake wote, washauri wake na vikosi vyake vyote, nitawatawanya nje kila upande. Nitauchomoa upanga na kuwafuatilia nyuma. Nitakapowatawanya kati ya mataifa mengine na nchi za mbali, ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Lakini nitawaacha wachache waokoke vitani, wanusurike njaa na maradhi mabaya; ili hao waweze kuwasimulia watu wa mataifa wanamoishi jinsi walivyotenda mabaya. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu, kula chakula na kunywa maji yako ukitetemeka kwa hofu. Waambie watu wa nchi hii, kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema juu ya wakazi wa Yerusalemu ambao bado wamo nchini Israeli, kwamba watakula chakula chao kwa hofu na watakunywa maji yao kwa kufadhaika, kwani nchi yao haitakuwa na kitu, kwa sababu kila mkazi ni mdhalimu. Miji yenye watu itateketezwa, na nchi itakuwa ukiwa. Nanyi mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu: Kwa nini methali hii inatajwa katika Israeli: ‘Siku zaja na kupita, lakini maono ya nabii hayatimii?’ Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema kwamba nitakomesha methali hiyo nao hawataitumia tena nchini Israeli. Waambie kuwa wakati umewadia ambapo maono yote yatatimia. Maana hapatakuwa tena na maono ya uongo au kupiga bao miongoni mwa Waisraeli. Mimi Mwenyezi-Mungu mwenyewe nitatangaza yatakayotukia. Nayo yatatukia bila kukawia. Wakati wa uhai wenu, enyi watu waasi, neno nitakalotamka nitalitimiza. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, Waisraeli wanafikiri kwamba maono yako yanahusu siku za baadaye sana, na unabii wako wahusu nyakati za mbali sana! Kwa hiyo waambie, kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema kuwa maneno yangu yote yatatimia karibuni. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema!” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, wakaripie manabii wa Israeli wanaotangaza mambo ambayo wameyafikiria wao wenyewe. Waambie wasikilize yale ambayo mimi Mwenyezi-Mungu ninasema. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Ole wenu manabii wapumbavu mnaofuata mawazo yenu wenyewe na maono yenu wenyewe! Manabii wenu, enyi Waisraeli ni kama mbweha wanaopitapita katika magofu. Hawakwenda kulinda sehemu zile za kuta zilizobomoka wala hawajengi kuta mpya ili Waisraeli waweze kujilinda wakati wa vita siku ile ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nimeiweka. Maono yao ni ya uongo mtupu na wanachotabiri ni udanganyifu mtupu. Hudai kwamba wanasema kwa niaba yangu mimi Mwenyezi-Mungu, lakini mimi sikuwatuma; kisha wananitazamia nitimize wanayosema. Basi, nawaulizeni: Je, maono yenu si uongo mtupu na utabiri wenu udanganyifu? Nyinyi mnadai kwamba mnasema kwa jina langu hali mimi sijaongea nanyi kamwe! “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa kuwa maneno yenu ni udanganyifu na maono yenu ni ya uongo mtupu, basi, mimi nitapambana nanyi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitanyosha mkono wangu dhidi yenu nyinyi manabii mnaotoa maono ya uongo na kutabiri udanganyifu mtupu. Watu wangu watakapokutanika kuamua mambo, nyinyi hamtakuwapo. Wala hamtakuwa katika orodha ya watu wa Israeli na hamtaingia katika nchi ya Israeli; ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu. Manabii hao wanawapotosha watu wangu na kuwaambia ‘Kuna amani’, wakati hakuna amani. Watu wangu wanajenga ukuta usiofaa, nao wanaupaka chokaa! Sasa waambie hao manabii wanaopaka chokaa ukuta huo kwamba itanyesha mvua kubwa ya mawe na dhoruba na ukuta huo utaanguka. Je, utakapoanguka, watu hawatawauliza: ‘Na ile chokaa mlioupaka iko wapi?’ Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Kwa ghadhabu yangu nitazusha upepo wa dhoruba na mvua nyingi ya mawe, navyo vitauangusha ukuta huo. Nitaubomolea mbali huo ukuta mlioupaka chokaa, na msingi wake utakuwa wazi. Ukuta huo ukianguka, mtaangamia chini yake. Ndipo mtakapotambua mimi ni Mwenyezi-Mungu. Hasira yangu yote nitaimalizia juu ya ukuta huo na juu ya hao walioupaka chokaa. Nanyi mtaambiwa: Ukuta haupo tena, wala walioupaka rangi hawapo; mwisho wa manabii wa Israeli waliotabiri mema juu ya Yerusalemu na kuona maono ya amani hali hakuna amani. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Na sasa, ewe mtu, wageukie wanawake wa taifa lako ambao wanatabiri mambo ambayo wameyawaza wao wenyewe. Tamka unabii dhidi yao na kuwaambia kuwa Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: Ole wenu wanawake mnaoshona tepe za hirizi za kuvaa mikononi mwa kila mtu na kutengeneza shela zenye hirizi za kila kimo ili kuyawinda maisha ya watu. Je, mnapowinda maisha ya watu wangu mnadhani mtasalimisha maisha yenu wenyewe? Mmenikufuru mbele ya watu wangu ili kupata konzi za shayiri na chakula kidogo. Mnawaua watu wasiostahili kufa na kuwaacha hai wanaostahili kuuawa, kwa uongo wenu mnaowaambia watu wangu, nao wanawaamini. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitashambulia hirizi zenu mnazowafunga nazo watu; nitazipasuapasua kutoka mikononi mwenu na kuwaacha huru hao mnaowawinda kama ndege. Nitazirarua shela zenu na kuwaokoa watu wangu mikononi mwenu; nao hawatakuwa tena mawindo mikononi mwenu. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Kwa kuwa mmewavunja moyo watu waadilifu kwa kusema uongo, hali mimi sikuwavunja moyo, mkawaimarisha waovu wasiache mienendo yao mibaya na kuokoa maisha yao, basi, nyinyi hamtaona tena maono madanganyifu, wala hamtatabiri tena. Nitawaokoa watu wangu mikononi mwenu. Hapo mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Siku moja baadhi ya wazee wa Israeli walinitembelea kutaka shauri. Basi neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu, watu hawa wamekubali mioyo yao itawaliwe na sanamu za miungu; miungu hiyo inawaelekeza kutenda dhambi. Je, nitakubali kuulizwa nao shauri? Basi, sema nao uwaambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli anayekubali sanamu za miungu zimtawale moyoni, na kuiruhusu miungu hiyo kumwelekeza kutenda dhambi, kisha akaja kumwomba shauri nabii, atapata jibu kutoka kwangu ambalo litazifaa hata sanamu zake nyingi za miungu. Nitaigusa mioyo ya Waisraeli ili wanirudie, kwani wamejitenga mbali nami kwa kuabudu sanamu zao za miungu. “Basi, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tubuni, na kuacha kuziabudu sanamu zenu za miungu. Acheni kufanya machukizo. Wakati wowote mmojawapo wa Waisraeli au mgeni yeyote akaaye katika Israeli, anapojitenga nami na kuanza kuziabudu sanamu za miungu kwa bidii na dhambi hiyo ikawa kizuizi kati yangu naye, halafu akamwendea nabii ili kujua matakwa yangu, basi, mimi Mwenyezi-Mungu mwenyewe, nitamjibu mtu huyo. Nitapambana naye. Nitamfanya kuwa ishara na kielelezo; nitamwondoa kabisa kutoka taifa langu. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Na ikiwa nabii huyo atadanganyika akasema kitu, basi mimi Mwenyezi-Mungu nimempotosha. Nami nitanyosha mkono wangu kumwondoa nabii huyo kutoka kwa watu wangu wa Israeli. Nitamwadhibu huyo nabii pamoja na huyo mtu aliyekuja kumwuliza matakwa yangu; wote watapata adhabu ileile, ili watu wa Israeli wasiniache tena na kujichafua wenyewe kwa kutenda dhambi; ili wawe watu wangu nami niwe Mungu wao. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Taifa fulani likitenda dhambi kwa kukosa uaminifu kwangu, mimi nitanyosha mkono wangu kuliadhibu. Nitaiondoa akiba yake ya chakula na kuliletea njaa. Nitawaua watu na wanyama wake. Hata kama Noa, Daneli na Yobu wangalikuwamo nchini humo, wangeyaokoa tu maisha yao wenyewe kwa uadilifu wao. Tena nitapeleka wanyama wa porini katika nchi hiyo na kuwanyanganya watoto wao na kuifanya nchi hiyo kuwa ukiwa, hata hakuna mtu yeyote atakayeweza kupita nchini humo kwa sababu ya wanyama wakali. Hata kama hao watu watatu mashuhuri wangalikuwamo nchini humo, naapa kwa jina langu, mimi Mwenyezi-Mungu, hawangeweza kuwaokoa watoto wao wenyewe; wao wenyewe tu wangeokolewa, lakini nchi hiyo ingekuwa ukiwa. Tena nitazusha vita dhidi ya nchi hiyo na kuamuru itokomezwe na kuulia mbali watu na wanyama. Na kama hao watu watatu wangalikuwamo nchini humo kweli hawangeweza kumwokoa hata mmoja wa watoto wao, wa kiume wala wa kike. Wangeweza tu kuokoa maisha yao wenyewe. Tena nitaleta maradhi mabaya nchini humo na kwa ghadhabu yangu nitawaua watu na wanyama. Na hata kama Noa, Danieli na Yobu wangelikuwa humo, kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, kweli hawangeweza kumwokoa hata mtoto wao mmoja wa kiume au wa kike. Wangeyaokoa tu maisha yao wenyewe kwa uadilifu wao. “Lakini mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Tena nitauadhibu Yerusalemu kwa mapigo yangu manne ya hukumu kali: Vita, njaa, wanyama wakali na maradhi mabaya, niwatokomeze humo watu na wanyama! Hata hivyo, wakibaki hai watu watakaonusurika na kuwaleta watoto wao wa kiume na wa kike kwako, wewe Ezekieli utaona jinsi walivyo waovu sana; nawe utakubali kwamba adhabu yangu juu ya Yerusalemu ni ya halali. Mienendo na matendo yao vitakuhakikishia kuwa maafa niliyouletea mji huo sikuyaleta bila sababu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Je, mti wa mzabibu ni bora kuliko miti mingine msituni? Je, mti wake wafaa kutengenezea kitu chochote? Je, watu huweza kutengeneza kigingi kutoka mti huo ili waweze kutundikia vitu? Huo wafaa tu kuwashia moto. Tena moto unapoteketeza sehemu yake ya mwanzo na ya mwisho na kuikausha sehemu ya katikati, je, hiyo yafaa kwa kitu chochote? Ulipokuwa haujachomwa ulikuwa haufai kitu, sembuse sasa baada ya kuteketezwa kwa moto na kuwa makaa! Haufai kitu kabisa. Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kama vile nilivyoutoa mti wa mzabibu kati ya miti ya msituni, ukateketezwa motoni, ndivyo nilivyotoa wakazi wa Yerusalemu. Nitawakabili vikali. Hata kama wataukimbia moto, huo moto utawateketeza. Hapo nitakapowakabili vikali, ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Kwa kuwa wamekosa uaminifu kwangu, nitaifanya nchi yao kuwa ukiwa. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, ujulishe mji wa Yerusalemu machukizo yake. Uuambie kuwa, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nauambia Yerusalemu: Kwa asili wewe ulizaliwa katika nchi ya Kanaani. Baba yako alikuwa Mwamori, na mama yako alikuwa Mhiti. Siku ile ulipozaliwa, kitovu chako hakikukatwa wala hukuoshwa kwa maji; hukusuguliwa kwa chumvi wala hukuvishwa nguo za kitoto. Hakuna aliyekuonea huruma na kukufanyia mambo hayo. Hakuna aliyekupenda. Bali, siku ile ulipozaliwa, ulitupwa huko mashambani kwa sababu siku ulipozaliwa ulichukiza sana. “Mimi nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nilikuambia, ‘Ishi, na ukue kama mmea shambani.’ Nawe ukakua na kurefuka hata ukawa msichana. Matiti yako yakakua na nywele zako nazo zikakua. Lakini ulikuwa uchi kabisa. “Nilipopita tena karibu nawe, nikakuona. Wakati huu, ulikuwa umefikia umri wa kupendwa kama msichana. Nikalitandaza vazi langu juu yako na kuufunika uchi wako. Nikafanya nawe agano la ndoa, nawe ukawa wangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Kisha nikachukua maji, nikakuosha damu uliyokuwa nayo, nikakupaka mafuta. Nilikuvika pia vazi lililonakshiwa na viatu vya ngozi. Nikakuzungushia kitambaa cha kitani safi na mtandio wa hariri. Nikakupamba kwa vito, nikakuvika bangili mikononi mwako na mkufu shingoni. Nikakutia hazama puani mwako, vipuli masikioni mwako na kichwani mwako nikakupamba kwa taji nzuri. Basi, ukapambika kwa dhahabu na fedha. Vazi lako likawa la kitani safi na hariri, nalo lilikuwa limenakshiwa. Ulitumia unga safi, asali na mafuta kwa chakula chako. Ukawa mzuri kupindukia, ukaifikia hali ya kifalme. Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kutokana na uzuri wako, kwani uzuri wako ulikamilika kwa sababu ya fahari niliyokujalia. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Lakini, ulitegemea uzuri wako, ukatumia sifa yako kwa kufanya uzinzi, ukifanya umalaya na mtu yeyote apitaye. Ulitwaa baadhi ya mavazi yako, ukayatumia kupambia mahali pako pa ibada na hapo ndipo ukafanyia uzinzi wako. Jambo la namna hiyo halijapata kutokea wala halitatokea kamwe! Vito vyako vizuri vya dhahabu na fedha nilivyokupa, ulivitwaa, ukajifanyia sanamu za wanaume upate kufanya uzinzi nazo. Ukatwaa mavazi niliyokupa yaliyotiwa nakshi na kuzifunika zile sanamu, na mafuta yangu na ubani wangu, ukazitolea sanamu hizo. Chakula changu nilichokupa, ulikitoa kwa sanamu hizo kuwa harufu ya kupendeza kwani nilikulisha kwa unga safi, mafuta na asali. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema! “Tena, watoto wako wa kiume na wa kike ulionizalia uliwatwaa, ukazitambikia sanamu zako kwa kuwateketeza. Je, unadhani uzinzi wako ulikuwa ni jambo dogo? Je, jambo hili la kuwachinja watoto wangu ili wawe tambiko ya kuteketeza kwa ajili ya sanamu zako ni jambo dogo? Katika machukizo yako yote pamoja na uzinzi wako hukuzikumbuka siku za utoto wako, wakati ulipokuwa uchi kabisa, bila kitu, ukigaagaa katika damu yako! “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia: Ole wako, ole wako Yerusalemu! Baada ya kufanya hayo yote ulijijengea majukwaa ya ibada na mahali pa juu kila mahali. Mwanzoni mwa kila barabara ulijijengea mahali pa juu, ukautumia urembo wako kufanya uzinzi ukijitoa kwa kila mpita njia na kuongeza uzinzi wako. Tena ulifanya uzinzi na jirani zako Wamisri waliojaa tamaa, ukaongeza uzinzi wako na kuichochea hasira yangu. Basi, niliunyosha mkono wangu kukuadhibu. Nilipunguza chakula chako, nikakuacha kwa maadui zako, binti za Wafilisti ambao waliona aibu mno juu ya tabia yako chafu mno. “Kwa kuwa hukutosheka, ulifanya tena uzinzi na Waashuru. Na hiyo pia haikukutosheleza. Ulijitoa wewe mwenyewe utumiwe na Wababuloni, watu wafanyao biashara! Hata hivyo hukutosheka. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema, kweli wewe ni mgonjwa wa mapenzi. Unafanya uzinzi bila kuona haya hata kidogo. Umejijengea jukwaa lako mwanzoni mwa kila barabara na kujijengea mahali pa juu katika kila mtaa. Tena wewe hukuwa kama malaya kwani ulikataa kulipwa. Ulikuwa mke mzinzi akaribishaye wageni badala ya mumewe. Kwa kawaida wanaume huwalipa malaya, lakini wewe umewalipa wapenzi wako wote, ukiwahonga waje kwako toka pande zote upate kuzini nao. Katika umalaya wako hukufanya kama wanawake wengine: Hakuna aliyekubembeleza ili uzini naye bali wewe ulilipa fedha badala ya kulipwa. “Sasa basi, ewe malaya, lisikie neno langu, mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia kwamba, wewe umetapanya fedha, umefunua uchi wako ili kuzini na wapenzi wako, umeziabudu sanamu zako zote za miungu na kuzitolea damu ya watoto wako. Basi, mimi nitawakusanya wapenzi wako wote uliojifurahisha nao, wote uliowapenda na wote uliowachukia. Nitawakusanya toka pande zote wakushambulie. Nitawafunulia uchi wako wapate kuuona. Nitakuhukumu kama wanavyohukumiwa wanawake wanaovunja ahadi ya ndoa au wauaji; nitakuhukumu kwa adhabu ya kifo kwa hasira na kwa ajili ya wivu. Nitakutia mikononi mwa wapenzi wako, nao watabomoa jukwaa lako na mahali pako pa ibada. Watakuvua mavazi yako na kukunyanganya vito vyako, wakuache uchi, bila kitu. Watakuletea jeshi kukushambulia; watakuua kwa kukupiga mawe na kisha watakukatakata kwa mapanga yao. Nyumba zako watazichoma moto na kuwafanya wanawake wengi waone adhabu yako. Utakoma kujitoa kwa mtu yeyote afanye uzinzi nawe. Hivyo, nitaitosheleza ghadhabu yangu juu yako, wivu niliokuwa nao juu yako utakwisha; nitatulia na wala sitaona hasira tena. Wewe umesahau yale ambayo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nilikufanyia ulipokuwa kijana. Wewe umenichukiza mno kwa mambo hayo yote. Basi, nitakulipiza kisasi kuhusu kila kitu ulichotenda. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Je, hukuongeza uchafu juu ya machukizo yako yote? “Ewe Yerusalemu! Mtu akitaka kutumia methali juu yako atasema: ‘Kama mama alivyo ndivyo alivyo binti yake.’ Kweli wewe ni mtoto wa mama aliyemchukia mumewe na watoto wake; wewe ni sawa na dada zako waliowachukia waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti na baba yako alikuwa Mwamori. Dada yako mkubwa ni Samaria, aliyekaa upande wako wa kaskazini mwako pamoja na binti zake. Dada yako mdogo ni Sodoma, aliyekaa upande wako wa kusini pamoja na binti zake. Lakini wewe hukutosheka kufuata mienendo yao au kutenda sawa na machukizo yao. Kwa muda mfupi tu ulipotoka kuliko walivyopotoka wao katika mienendo yako yote. Kweli naapa kwa nafsi yangu, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu kuwa, dada yako Sodoma na binti zake, hawakufanya maovu kama yale uliyotenda wewe na binti zako. Kosa la dada yako Sodoma, lilikuwa hili: Yeye pamoja na binti zake walipokuwa na chakula na fanaka tele, walianza kujivuna, wakaacha kuwasaidia maskini na fukara. Walijivuna, wakafanya machukizo mbele yangu. Kwa hiyo niliwaangamiza mara tu nilipoyaona hayo. Naye Samaria kwa kweli hakutenda hata nusu ya dhambi zako. Wewe umefanya machukizo mengi kuliko wao. Ukilinganisha maovu yako na ya dada zako, maovu yao si kitu! Wewe utaibeba aibu yako kabisa! Dhambi zako ni mbaya zaidi kuliko za dada zako, kiasi cha kuwafanya dada zako na dhambi zao waonekane hawana hatia. Basi, ona aibu na kubeba fedheha yako, maana umewafanya dada zako waonekane hawana hatia. “Nitawarudishia Sodoma na Samaria pamoja na binti zao fanaka yao ya awali. Nawe pia nitakufanikisha miongoni mwao, ili ubebe aibu yako na kuona haya, kwa sababu ya mambo yote uliyotenda, ndipo kwa hali yako hiyo dada zako watajiona kwamba wao ni afadhali. Dada zako, Sodoma na Samaria, pamoja na binti zao watairudia hali yao ya hapo awali. Hata wewe na binti zako mtairudia hali yenu. Kwa majivuno yako ulimdharau dada yako Sodoma. Je, hukufanya hivyo kabla uovu wako haujafichuliwa? Sasa umekuwa kama Sodoma. Umekuwa kitu cha dhihaka mbele ya binti za Edomu na jirani zake wote, na binti za Wafilisti jirani zako ambao walikuchukia. Adhabu ya uchafu wa tabia na machukizo yako utaibeba wewe mwenyewe. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Naam! Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitakutenda wewe Yerusalemu kama unavyostahili. Wewe umekidharau kiapo chako, ukavunja na lile agano. Lakini mimi nitalikumbuka agano langu nililoagana nawe katika siku za ujana wako. Nitafanya nawe agano la milele. Nawe utakumbuka mienendo yako na kuona aibu wakati nitakapokupa dada zako, mkubwa na mdogo, kama binti zako, ingawa si kwa sababu ya agano kati yangu na wewe. Mimi nitafanya agano nawe, nawe utatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nitakusamehe kila kitu ulichotenda. Nawe utakapokumbuka hayo yote uliyotenda utashangaa na kunyamaza kwa aibu wala hutathubutu kusema tena. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Tega kitendawili, uwaambie fumbo Waisraeli. Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kulikuwa na tai mmoja mkubwa sana aliyekuwa na mabawa makubwa, yenye manyoya marefu mengi yenye rangi za kila aina. Tai huyo aliruka mpaka mlimani Lebanoni, akatua juu ya kilele cha mwerezi; akakwanyua tawi lake la juu zaidi, akalipeleka katika nchi ya wafanyabiashara, akaliweka katika mji wao mmoja. Kisha akachukua mmea mchanga nchini Israeli, akaupanda katika ardhi yenye rutuba ambako kulikuwa na maji mengi. Mmea ukakua ukawa mzabibu wa aina ya mti utambaao; matawi yake yakamwelekea, na mizizi yake ikatanda chini yake. Mzabibu ukachipua matawi na majani mengi. Lakini kulikuwa na tai mwingine mkubwa; alikuwa na mabawa makubwa ya manyoya mengi. Basi, ule mzabibu ukamtandia mizizi yake, ukamwelekezea matawi yake, ili aumwagilie maji. Mzabibu ulikuwa umetolewa kitaluni mwake ukapandikizwa penye udongo mzuri na maji mengi, ili upate kutoa matawi na kuzaa matunda uweze kuwa mzabibu mzuri sana! Sasa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuuliza: Je, mzabibu huo utaweza kustawi? Je, hawatangoa mizizi yake na kuozesha matunda yake na matawi yake machanga kuyanyausha? Hakutahitajika mtu mwenye nguvu au jeshi kuungoa kutoka humo ardhini. Umepandikizwa, lakini, je, utastawi? Upepo wa mashariki uvumapo juu yake utanyauka; utanyauka papo hapo kwenye kuta ulikoota.” Kisha neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Sasa waulize hao watu waasi kama wanaelewa maana ya mfano huo. Waambie kuwa, mfalme wa Babuloni alikuja Yerusalemu, akamwondoa mfalme na viongozi wake, akawapeleka Babuloni. Kisha akamtawaza mmoja wa jamaa ya kifalme, akafanya naye mapatano, akamwapisha. Aliwaondoa humo nchini watu mashujaa akawapeleka mbali ili utawala huo uwe dhaifu na uzingatie agano lake mfalme wa Babuloni. Lakini yule mfalme mpya alimwasi mfalme wa Babuloni kwa kuwatuma wajumbe Misri kuomba farasi na askari wengi. Je, mfalme huyo atafaulu? Je, anayefanya hivyo na kuvunja agano lake ataweza kuepa adhabu? “Mimi Mwenyezi-Mungu naapa kwamba, kama niishivyo, mfalme huyu atafia katika nchi ya Babuloni, nchi ya mfalme yule aliyemweka awe mfalme, na ambaye amedharau kile kiapo na kuvunja lile agano alilofanya naye. Hakika, Farao pamoja na jeshi lake kubwa hataweza kumsaidia vitani wakati Wababuloni watakapomzungushia ngome na kuta ili kuwaua watu wengi. Kwa kuwa alikidharau kile kiapo na kuvunja lile agano ambalo aliahidi kwa mkono wake mwenyewe na kufanya mambo haya yote, hakika hataokoka. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema, kama niishivyo, kwa vile amekidharau kiapo alichoapa kwa jina langu na agano langu akalivunja, hakika nitamwadhibu vikali. Nitatandaza wavu wangu juu yake, naye atanaswa katika mtego wangu; nitampeleka mpaka Babuloni na kumhukumu kwa sababu ya uhaini alioufanya dhidi yangu. Majeshi yake hodari yatauawa kwa upanga na watakaosalia hai watatawanyika pande zote. Hapo mtatambua kuwa mimi, naam, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi mwenyewe nitachukua kisehemu cha ncha ya juu ya mwerezi, naam, nitavunja tawi changa kutoka matawi yake ya juu na kulipanda juu ya mlima mrefu sana. Naam, nitalipanda juu ya mlima mrefu wa Israeli ili lichanue na kuzaa matunda. Litakuwa mwerezi mzuri, na ndege wa aina zote watakaa chini yake pia watajenga viota vyao katika matawi yake. Ndipo miti yote nchini itajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu huiporomosha miti mirefu na kuikuza miti mifupi. Mimi hukausha miti mibichi na kustawisha miti mikavu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema hayo na nitayafanya.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Kwa nini mnarudiarudia methali hii katika nchi ya Israeli: ‘Akina baba wamekula zabibu mbichi, lakini meno ya watoto wao yakatiwa ganzi!’ Lakini, kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nasema kwamba methali hii haitatumika tena katika Israeli. Jueni kwamba uhai wote ule ni wangu, uhai wa mzazi na uhai wa mtoto. Yeyote anayetenda dhambi, ndiye atakayekufa. “Kama mtu ni mwadilifu, anafuata yaliyo haki na sawa, kama hashiriki tambiko za sanamu za miungu mlimani wala kuzitegemea sanamu za miungu ya Waisraeli, kama hatembei na mke wa jirani yake wala kulala na mwanamke wakati wa siku zake, kama hamdhulumu mtu yeyote, bali hurudisha rehani, kama hanyanganyi watu mali zao, bali huwapa chakula wenye njaa na kuwavalisha walio uchi, kama hakopeshi kwa riba, wala kujipatia ziada, kama hafanyi uovu wowote, ila anaamua kwa haki kati ya mdai na mdaiwa, kama anafuata kanuni zangu na kutii sheria zangu kwa dhati, mtu huyo ndiye mwadilifu; naye hakika ataishi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Ikiwa mtu huyo ana mtoto mkatili au muuaji, mtoto huyo ambaye anafanya mabaya asiyofanya baba yake: Anakula tambiko zilizokatazwa huko mlimani, anamnajisi mke wa jirani yake, anawadhulumu maskini na fukara, anaiba, harudishi rehani, anaziabudu sanamu za miungu na kufanya machukizo, anakopesha kwa riba na kujitafutia ziada, je, mtoto huyo ataishi? La, hataweza kuishi. Kwa kuwa amefanya machukizo yote hayo, hakika atakufa, na yeye mwenyewe atawajibika kwa kifo chake. “Lakini kama mtu huyo akiwa na mtoto ambaye ameona dhambi alizotenda baba yake, lakini yeye hatendi mabaya hayo, hali tambiko zilizokatazwa huko mlimani, wala kuziabudu sanamu za miungu ya Waisraeli, hamnajisi mke wa jirani yake, hampunji mtu yeyote, hashiki rehani, hanyanganyi watu mali zao, bali huwapa chakula wenye njaa na kumvalisha aliye uchi, huepa kutenda uovu, hakopeshi kwa riba, wala kujitafutia ziada, huzifuata amri na maagizo yangu; huyo hatakufa kwa sababu ya uovu wa baba yake. Huyo ataishi. Lakini baba yake, kwa sababu alitoza bei isiyo halali na kumwibia ndugu yake, wala hakuwatendea ndugu zake wema, hakika atakufa kwa sababu ya uovu wake. “Lakini mnauliza, ‘Kwa nini mtoto asiadhibiwe kwa sababu ya dhambi za baba yake?’ Mtoto akitenda yaliyo ya haki na sawa, kama akiwa mwangalifu kuzingatia kanuni zangu zote, basi, huyo hakika ataishi. Atakayetenda dhambi ndiye atakayekufa. Mtoto hatawajibika kwa uovu wa baba yake, wala baba hatawajibika kwa uovu wa mtoto wake. Uadilifu wa mwadilifu utamfaa yeye mwenyewe: Na uovu wa mwovu ataubeba yeye mwenyewe. “Kama mtu mwovu akiachana na dhambi zake zote alizotenda, kama akishika kanuni zangu zote, akatenda yaliyo ya haki na sawa, huyo hakika ataishi, hatakufa. Makosa yake yote aliyofanya hayatakumbukwa; kwa sababu ya uadilifu wake ataishi. Je, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nafurahia kufa kwake mtu mwovu? La hasha! Mimi napendelea aachane na njia zake mbaya apate kuishi. “Lakini, mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake, akatenda uovu na kufanya machukizo yaleyale anayofanya mtu mwovu, je, huyo ataishi? La! Matendo yake yote mema aliyotenda hayatakumbukwa tena; atakufa kwa sababu ya uasi na dhambi aliyotenda. “Lakini nyinyi mwasema, ‘Hicho afanyacho Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Sikilizeni sasa, enyi Waisraeli: Je, ninachofanya mimi si sawa? Mnachofanya nyinyi ndicho kisicho sawa. Mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake na kutenda uovu atakufa kwa ajili hiyo; atakufa kwa sababu ya uovu aliotenda. Lakini mtu mwovu akiachana na uovu aliofanya, akatenda mambo yaliyo haki na sawa, huyo atayaokoa maisha yake. Kwa kuwa amefikiri, akaachana na makosa aliyoyafanya, hakika ataishi; hatakufa. Lakini nyinyi Waisraeli mwasema, ‘Anachotenda Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Enyi Waisraeli, je, ninachofanya mimi si sawa? Mnachofanya nyinyi ndicho kisicho sawa. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nasema hivi: Nitawahukumu nyinyi Waisraeli, kila mmoja wenu, kulingana na mwenendo wake. Tubuni na kuachana na makosa yenu, yasije yakawaangamiza. Tupilieni mbali dhambi mlizonitendea; jipatieni moyo na roho mpya. Enyi Waisraeli, ya nini mfe? Sifurahii kifo cha mtu yeyote. Hivyo tubuni ili mpate kuishi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mungu aliniambia niimbe utenzi huu wa maombolezo kuhusu wakuu wa Israeli: Mama yenu alikuwa simba wa fahari miongoni mwa simba wengine. Alikaa kati ya simba vijana, akawalisha watoto wake. Alimlea mtoto mmojawapo wa watoto wake, mtoto huyo naye akawa simba kijana hodari. Akajifunza kwa mama yake kuwinda, akawa simba mla watu. Mataifa yakapiga mbiu ya hatari dhidi yake, wakamnasa katika mtego wao, wakampeleka kwa ndoana mpaka Misri. Mama yake alipoona kuwa amechoka kungoja, matumaini ya kumpata yamekwisha, alimchukua mtoto wake mwingine, akamfanya simba kijana hodari. Huyo alipokuwa amekua, akaanza kuzurura na simba wengine. Naye pia akajifunza kuwinda, akawa simba mla watu. Aliziandama ngome za watu na kuiharibu miji yao. Nchi ikatishika pamoja na wakazi wake, kwa sauti ya kunguruma kwake. Mataifa yakamkabili kutoka mkoani mwao kote, wakatandaza wavu wao juu yake, naye akanaswa katika mtego wao. Kwa ndoana wakamtia katika kizimba chao, wakampeleka kwa mfalme wa Babuloni. Huko, wakamtia gerezani, ili ngurumo yake isisikike tena juu ya milima ya Israeli. Mama yako alikuwa kama mzabibu shambani, uliopandikizwa kando ya maji, ambao ulizaa sana kwa kuwa na maji tele. Ulikuwa na matawi yenye nguvu, ambayo yalikuwa fimbo za kifalme. Mzabibu huo ulikua kupita miti mingine, watu waliusifu ukubwa wa shina lake na wingi wa matawi yake. Lakini ulingolewa kwa hasira ukatupwa chini ardhini; upepo wa mashariki ukaukausha, matunda yake yakapukutika; matawi yake yenye nguvu yalikaushwa, nao moto ukauteketeza. Na sasa umepandikizwa jangwani, katika nchi kame isiyo na maji. Lakini moto umetoka kwenye shina lake, umeyateketeza matawi na matunda yake. Matawi yake kamwe hayatakuwa na nguvu, wala hayatakuwa fimbo za kifalme. Huo umekuwa wimbo wa maombolezo; ndivyo unavyoimbwa daima. Mwaka wa saba tangu kuhamishwa kwetu, siku ya kumi ya mwezi wa tano, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja kumwuliza Mwenyezi-Mungu shauri, wakaketi mbele yangu. Basi, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu, sema na hao wazee wa Israeli. Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Je, mmekuja kuniuliza shauri? Hakika, kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nasema kuwa sitakubali kuulizwa kitu na nyinyi. “Wewe mtu, je, uko tayari kuwahukumu watu hawa? Basi, wahukumu. Wajulishe waliyofanya wazee wao. Waambie kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile nilipowachagua Waisraeli niliwaapia wazawa wa Yakobo. Nilijidhihirisha kwao nchini Misri, nikawaapia nikisema: Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Siku hiyo niliwaapia kwamba nitawatoa nchini Misri na kuwaongoza mpaka kwenye nchi niliyowachagulia, nchi inayotiririka maziwa na asali na nchi nzuri kuliko nchi zote. Niliwaambia: ‘Tupilieni mbali machukizo yote mnayoyapenda; msijitie unajisi kwa sanamu za miungu ya Misri, kwa maana mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.’ Lakini waliniasi, hawakutaka kunisikiliza. Hakuna hata mmoja wao aliyetupilia mbali machukizo yale waliyoyapenda, wala hawakuachana na sanamu za miungu ya Misri. Basi, nikafikiri kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuitimiza hasira yangu juu yao wakiwa kulekule nchini Misri. Lakini nilijizuia kufanya hivyo kwa heshima ya jina langu ili lisidharauliwe kati ya watu wa mataifa wanaoishi nao, hao walioona nikijijulisha kwa Waisraeli wakati wa kuwatoa katika nchi ya Misri. “Basi, mimi niliwatoa nchini Misri, nikawapeleka jangwani. Niliwapa kanuni zangu na kuwafundisha amri zangu ambazo mtu akizifuata huishi. Niliwapa pia Sabato zangu ziwe ishara kati yangu na wao, wapate kujua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu ninayewatakasa. Lakini Waisraeli waliniasi huko jangwani; hawakuzifuata kanuni zangu, bali walizikataa sheria zangu ambazo mtu akizifuata huishi. Sabato zangu walizikufuru daima, nami nikasema kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuwaangamiza hukohuko jangwani. Lakini nilijizuia kufanya hivyo kwa sababu ya heshima ya jina langu ili nisidharauliwe kati ya watu wa mataifa ambao walishuhudia jinsi nilivyowatoa Waisraeli nchini Misri. Hata hivyo, niliwaapia kulekule jangwani kwamba sitawaingiza katika nchi niliyowapa, nchi inayotiririka maziwa na asali na nchi nzuri kuliko nchi zote. Nilifanya hivyo kwa sababu walizikataa kanuni zangu na kuzikufuru Sabato zangu; kwani walipania kwa moyo sanamu za miungu yao. Lakini nilisalimisha maisha yao, sikuwaangamiza kule jangwani. “Niliwaonya wazawa wao kule jangwani: ‘Msizifuate desturi za wazee wenu, msishike amri zao wala msijitie unajisi kwa kuziabudu sanamu za miungu yao. Mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu. Fuateni kanuni zangu, shikeni amri zangu kwa uangalifu. Fanyeni Sabato zangu kuwa takatifu, ili ziwe ishara ya agano langu nanyi. Hizo zitawakumbusha kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu.’ “Lakini hata wazawa wao hao waliniasi. Hawakufuata kanuni zangu, hawakushika wala kutekeleza amri zangu ambazo mtu akizishika, huishi. Walizikufuru Sabato zangu. Basi nikasema kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuitimiza hasira yangu juu yao huko jangwani. Lakini nilizuia mkono wangu kwa sababu ya heshima ya jina langu ili nisidharauliwe kati ya watu wa mataifa walioona nikiwatoa nchini Misri. Hata hivyo, niliapa hukohuko jangwani kuwa ningewapeleka katika nchi za mbali na kuwafanya waishi miongoni mwa mataifa ya kigeni, kwa sababu hawakufuata amri zangu, bali walizikataa kanuni zangu, wakazikufuru Sabato zangu na kuziabudu sanamu za miungu ya wazee wao. “Tena niliwapa kanuni mbaya na amri ambazo mtu akizifuata hataishi. Nikawaacha watiwe unajisi kwa tambiko zao za kuwatoa wazaliwa wao wa kwanza kafara kwa sanamu za miungu. Hili lilikuwa pigo lao la adhabu ya kutisha ili watambue kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Sasa, wewe mtu, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Wazee wenu walinikufuru kila mara kwa kukosa uaminifu. Maana nilipowapeleka katika ile nchi niliyoapa kuwapa, kila walipoona kilima kirefu au miti ya majani mengi, walianza kutoa matambiko na tambiko zao na kunichokoza. Hukohuko walitoa tambiko za harufu nzuri na kumimina tambiko za kinywaji. (Mimi nikawauliza, ‘Mahali hapo palipoinuka mnapokwenda panaitwaje?’ Wao wakapaita ‘Mahali palipoinuka’ mpaka leo.) Basi, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawauliza hivi: Je, mtajitia unajisi kwa kufuata desturi za wazee wenu na kuviabudu vitu vinavyonichukiza? Mnapoendelea kutoa tambiko zenu na kuwapitisha watoto wenu motoni mnajitia unajisi mpaka leo hii. Je, nitaulizwa shauri nanyi, enyi watu wa Israeli? Lakini, kama niishivyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu naapa kwamba sitakubali kuulizwa shauri nanyi. Nyinyi mnasema mioyoni mwenu, ‘Tutakuwa kama mataifa mengine, kama makabila ya nchi nyingine na kuabudu miti na mawe.’ Hayo mnayopania mioyoni mwenu hayatafanikiwa kamwe. “Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba mimi nitawatawala kwa mkono wenye nguvu, kwa ukali na kuwamwagia ghadhabu yangu. Nitawatoa kutoka mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa kwa mkono wangu wenye nguvu, kwa ukali na kwa ghadhabu yangu. Nitawapeleka kwenye jangwa la mataifa; na huko nitawahukumu moja kwa moja. Kama nilivyowahukumu wazee wenu kule jangwani katika nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu nyinyi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitawalazimisha muwe chini ya uchungaji wangu kila mmoja, na kuwafanya mlitii agano langu. Nitaondoa miongoni mwenu waasi na wale wanaonikosea; nitawaondoa katika nchi walikokaa kama wakimbizi, lakini nchi ya Israeli hawataiingia kamwe. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Na sasa, enyi Waisraeli, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambia hivi: Haya! Endeleeni kuziabudu sanamu zenu za miungu, kama hamnisikilizi; lakini mtalazimika kuacha kulikufuru jina langu takatifu kwa tambiko na sanamu zenu. Maana, katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, natamka mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nyinyi nyote watu wa Israeli mtanitumikia huko. Huko mimi nitawapokeeni na kungojea mniletee huko sadaka na tambiko zenu bora na matoleo mliyoyaweka wakfu. Baada ya kuwatoa katika nchi ambako mmetawanywa na kuwakusanya pamoja, nitazipokea tambiko zenu za harufu nzuri. Nami nitadhihirisha utakatifu wangu kati yenu mbele ya mataifa mengine. Nanyi mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, wakati nitakapowaleta mpaka katika nchi ya Israeli, nchi niliyoapa kuwapa wazee wenu. Huko ndiko mtakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu mabaya ambayo yaliwatieni unajisi; nanyi mtachukizwa kabisa kwa sababu ya maovu yote mliyotenda. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, wakati nitakapowatendea nyinyi sio kulingana na mwenendo wenu na matendo yenu mabaya, bali kwa heshima ya jina langu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, geukia upande wa kusini uhubiri dhidi ya nchi ya kusini, dhidi ya wakazi wa msitu wa Negebu. Waambie wasikilize neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitawasha moto kwako, nao utateketeza miti yote, mibichi na mikavu; utaenea tangu kusini mpaka kaskazini wala hakuna atakayeweza kuzima miali yake. Kila mtu atausikia mchomo wake. Watu wote watajua kwamba ni mimi Mwenyezi-Mungu niliyeuwasha na hautazimika.” Kisha nami nikasema, “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu! Watu wanalalamika juu yangu na kusema: ‘Huyu akisema, ni mafumbo tu!’” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, ugeukie mji wa Yerusalemu, uhubiri dhidi ya sehemu zake za ibada, na kutoa unabii juu ya nchi ya Israeli. Waambie Waisraeli kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe naja kupambana nanyi. Nitauchomoa upanga wangu alani mwake na kuwaua watu wema na wabaya. Tangu kaskazini hadi kusini, nitawakatilia mbali watu wote, wema na wabaya, kwa upanga wangu. Watu wote watajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndiye niliyeuchomoa upanga alani mwake na wala hautarudishwa tena ndani. “Nawe mtu, jikunje kama mtu aliyekata tamaa, uomboleze mbele yao. Wakikuuliza, ‘Kwa nini unaomboleza?’ Utawaambia: ‘Naomboleza kwa sababu ya habari zinazokuja.’ Kila mtu atakufa moyo, mikono yao yote italegea; kila aishiye atazimia na magoti yao yatakuwa kama maji. Habari hizo zaja kweli, nazo zinatekelezwa. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, toa unabii useme: Mwenyezi-Mungu asema hivi: Upanga! Naam, upanga umenolewa, nao umengarishwa pia. Umenolewa ili ufanye mauaji, umengarishwa umetamete kama umeme! Umenolewa na kungarishwa uwekwe mkononi mwa mwuaji. Wewe mtu, lia na kuomboleza upanga huo umenyoshwa dhidi ya watu wangu, dhidi ya wakuu wote wa Israeli. Wataangamizwa kwa upanga pamoja na watu wangu. Jipige kifua kwa huzuni. Hilo litakuwa jaribio gumu sana. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wewe mtu, tabiri! Piga makofi, upanga na ufanye kazi yake, mara mbili, mara tatu. Huo ni upanga wa mauaji nao unawazunguka. Kwa hiyo wamekufa moyo na wengi wanaanguka. Ncha ya upanga nimeiweka katika malango yao yote. Umefanywa ungae kama umeme, umengarishwa kwa ajili ya mauaji. Ewe upanga, shambulia kulia, shambulia kushoto; elekeza ncha yako pande zote. Nami nitapiga makofi, nitatosheleza ghadhabu yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Chora njia mbili ambapo utapitia upanga wa mfalme wa Babuloni. Njia zote mbili zianzie katika nchi moja. Mwanzoni mwa kila njia utaweka alama ya kuonesha upande mji uliko. Utachora njia upanga utakapopitia kwenda kuufikilia mji wa Raba wa Waamoni, na njia nyingine inayoelekea mji wenye ngome wa Yerusalemu nchini Yuda. Mfalme wa Babuloni anasimama mwanzoni mwa hizo njia mbili, kwenye njia panda, apate kupiga bao. Anatikisa mishale, anaviuliza shauri vinyago vya miungu yake na kuchunguza maini ya mnyama. Mshale unaodokezea ‘Yerusalemu’ umeangukia mkono wake wa kulia. Anaweka zana za kubomolea, anaamuru mauaji na kelele za vita zifanywe, zana za kubomolea malango zimewekwa, maboma na minara ya kuuzingira mji vimewekwa. Lakini watu wa Yerusalemu wataudhania kuwa ni utabiri wa uongo kwa sababu wamekula kiapo rasmi. Hata hivyo unabii huu utawakumbusha uovu wao na kusababishwa kukamatwa kwao. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wote wataweza kuziona dhambi zenu. Kila mtu atajua jinsi mlivyo na hatia. Kila kitendo mnachotenda kinaonesha dhambi zenu. Nyinyi mmehukumiwa adhabu nami nitawatia mikononi mwa maadui zenu. “Nawe mtawala wa Israeli wewe ni mpotovu kabisa. Siku yako imefika, naam, siku ya adhabu yako ya mwisho. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia hivi: Vua kilemba chako na taji yako kwani mambo hayatabaki kama yalivyokuwa. Walio chini watakwezwa, walio juu watashushwa! Uharibifu! Uharibifu! Hamna chochote katika mji huu nitakachosaza. Lakini kabla ya hayo atakuja yule ambaye nimempa mamlaka ya kuuadhibu, ambaye mimi nitampa mji huo. “Ewe mtu, tabiri kuhusu Waamoni na maneno yao ya dhihaka kwa Waisraeli: Waambie kuwa nasema: Upanga, upanga! Upanga umenyoshwa kuua, umenolewa uangamize, umengarishwa ungae kama umeme. Wakati nyinyi mmetulia katika maono yenu madanganyifu na utabiri wenu wa uongo, upanga utakuwa tayari kukata shingo za waasi na waovu. Siku imewadia ambapo maovu yenu yataadhibiwa. “Sasa rudisha upanga alani mwake! Nitawahukumu mahali palepale mlipoumbwa, katika nchi mlipozaliwa. Nitawamwagia ghadhabu yangu. Moto wa ghadhabu yangu nitaupuliza juu yenu. Nitawatia mikononi mwa watu wakatili, watu hodari wa kuangamiza. Mtakuwa kuni motoni, damu yenu itamwagika katika nchi. Mtu hatawakumbuka tena. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Ewe mtu! Uko tayari kutoa hukumu, kuuhukumu mji huu wa wauaji? Basi, ujulishe machukizo yake yote. Uambie, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe ni mji unaowaua watu wako mwenyewe na kujitia unajisi kwa kufanya sanamu za miungu; kwa hiyo wakati wako wa adhabu umewadia. Una hatia kutokana na damu uliyomwaga. Umejifanya najisi kwa sanamu ulizojifanyia. Siku yako ya adhabu umeileta karibu nawe; naam, siku zako zimehesabiwa. Ndio maana nimekufanya udhihakiwe na mataifa na kudharauliwa na nchi zote. Nchi zote za mbali na karibu zitakudhihaki. Umejipatia sifa mbaya na kujaa fujo. “Wakuu wa Israeli walioko kwako, kila mmoja kadiri ya nguvu zake huua watu. Kwako baba na mama wanadharauliwa. Mgeni anayekaa kwako anapokonywa mali yake. Yatima na wajane wanaonewa. Wewe umedharau vyombo vyangu vitakatifu na kuzikufuru sabato zangu. Kwako wamo wanaowasingizia wengine ili wauawe. Wakazi wako hushiriki chakula kilichotolewa kwa miungu milimani. Watu wako wanatenda ufisadi. Kwako wamo watu ambao hulala na wake za baba zao. Huwanajisi wanawake katika siku zao za hedhi. Wengine hufanya machukizo kwa kulala na wake za majirani zao. Wengine hulala na wake za watoto wao, na wengine hulala na dada zao. Huko kwako kuna watu ambao huua kwa malipo. Umepokea riba na kuwalangua wenzako ili kujitajirisha, na kunisahau mimi kabisa! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nimekunja ngumi yangu dhidi yako kwa sababu ya hiyo faida uliyopata kwa njia isiyo halali na kwa mauaji yaliyofanyika kwako. Je, utaweza kustahimili kuwa hodari siku nitakapopambana nawe? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema na nitayatekeleza hayo. Nitakutawanya kati ya mataifa na kukutupatupa katika nchi nyingine. Nitaukomesha uchafu ulioko kwako. Utajiweka najisi mbele ya mataifa mengine, lakini utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Tena neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu! Waisraeli wamekuwa kwangu kama takataka. Wao ni kama takataka inayosalia wakati madini ya shaba, bati, chuma au risasi yanaposafishwa. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa kuwa nyinyi nyote mmekuwa takataka ya madini, mimi nitawakusanya pamoja mjini Yerusalemu. Kama watu wanavyokusanya fedha, shaba, chuma, risasi na bati katika tanuri ili kuzisafisha kwa kuchoma moto, ndivyo ghadhabu na hasira yangu itakavyowakusanya huko na kuwayeyusha. Nitawakusanya na kuwawasha moto kwa ghadhabu yangu; nanyi mtayeyushwa mkiwa humo mjini. Kama fedha iyeyushwavyo katika tanuri, ndivyo mtakavyoyeyushwa humo mjini. Nanyi mtatambua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nimeimwaga ghadhabu yangu juu yenu.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Waambie Waisraeli kwamba nchi yao ni kama nchi ambayo haijanyeshewa mvua, imenyauka kwa sababu ya ghadhabu yangu ikawa kama ardhi bila maji. Wakuu wenu ni kama simba anayenguruma araruapo mawindo yake. Wanaua watu, wanawanyanganya watu mali na johari, na kuongeza idadi ya wajane. Makuhani wao wanavunja sheria zangu, na kukufuru vyombo vyangu vitakatifu. Hawapambanui kati ya vitu vitakatifu na vitu visivyo vitakatifu, wala hawawafundishi watu tofauti kati ya mambo yaliyo najisi na yaliyo safi. Wameacha kuzishika sabato zangu, na kunifanya nidharauliwe kati yao. Viongozi wake waliomo mjini ni kama mbwamwitu wararuao mawindo yao; wanaua ili kujitajirisha visivyo halali. Manabii wake wanaficha maovu hayo kama mtu anapotia chokaa kwenye ukuta mbovu. Wanaona maono ya uongo na kutabiri udanganyifu mtupu, wakisema, ‘Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi,’ wakati mimi mwenyewe sijawaambia chochote. Kila mahali nchini ni dhuluma na unyanganyi. Wanawadhulumu maskini na wanyonge, na kuwaonea wageni bila kujali. Nilitafuta miongoni mwao mtu mmoja atengeneze ukuta na kusimama juu ya mahali palipobomoka mbele yangu, ili ailinde nchi na kunizuia nisiiharibu, lakini sikumpata hata mmoja. Kwa hiyo nimewamwagia ghadhabu yangu na kwa moto wa hasira yangu nimewateketeza kulingana na matendo yao. Ndivyo nisemavyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Palikuwa na binti wawili, wote wa mama mmoja. Walipokuwa vijana tu, wakiwa wanakaa kule Misri, wakakubali matiti yao kutomaswa, wakapoteza ubikira wao, wakawa malaya. Yule mkubwa aliitwa Ohola, na yule mdogo Oholiba. Basi, wote wakawa wangu, wakanizalia watoto, wa kiume na wa kike. Basi, Ohola ni Samaria na Oholiba ni Yerusalemu! “Ingawa Ohola alikuwa mke wangu, lakini aliendelea kuwa mzinzi na kuwatamani wapenzi wake wa Ashuru. Hao walikuwa askari, wamevalia sare za rangi ya zambarau, watawala na makamanda. Wote walikuwa vijana wa kuvutia na wapandafarasi hodari. Ohola alifanya zinaa na hao maofisa wote wa vyeo vya juu wa Ashuru naye akajitia unajisi kwa vinyago vyote vya kila mwanamume wake aliyemtamani. Aliendelea na uzinzi wake aliouanza kule Misri wakati huo, akiwa bado kijana, wanaume walivunja ubikira wake na kuzitimiza tamaa zao kwake. Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa Waashuru wapenzi wake, ambao aliwatamani sana. Hao walimvua mavazi yake na kumwacha uchi. Waliwakamata watoto wake, naye mwenyewe wakamuua kwa upanga. Adhabu hiyo aliyopata ikawa fundisho kwa wanawake wengine. “Oholiba dada yake, aliona jambo hilo, lakini akawa amepotoka kuliko yeye katika tamaa yake na uzinzi wake uliokuwa mbaya kuliko wa dada yake. Aliwatamani sana Waashuru: Wakuu wa mikoa, makamanda, wanajeshi waliovaa sare zao za kijeshi, wapandafarasi hodari, wote wakiwa vijana wa kuvutia. Nilimtambua kuwa najisi. Ama kweli wote wawili walikuwa na tabia hiyo moja. Lakini Oholiba alizidisha uzinzi wake; akapendezwa na picha za Wakaldayo zilizochorwa ukutani, zimetiwa rangi nyekundu, mikanda viunoni, vilemba vikubwa vichwani; hizo zote zilifanana na maofisa, naam, picha ya Wababuloni, wakazi wa nchi ya Wakaldayo. Alipoziona picha hizo, mara akashikwa na tamaa, akatuma wajumbe kwenda Ukaldayo. Basi, Wababuloni wakaja kulala naye. Wakamtia najisi kwa tamaa zao. Alipokwisha tiwa najisi, akajitenga nao. Alipoendelea na uzinzi wake na kufunua uchi wake, mimi nilimwacha kama nilivyomwacha dada yake. Hata hivyo, akazidisha uzinzi wake akifanya kama wakati wa ujana wake alipofanya uzinzi kule Misri. Aliwatamani sana wanaume wenye tamaa mbaya kama ya punda na nguvu nyingi za uzazi kama farasi dume.” “Oholiba aliutamani uchafu wake wa ujana alipokuwa Misri, ambako Wamisri walivunja ubikira wake, na kuyatomasa matiti yake machanga. “Sasa Oholiba! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawafanya wapenzi wako uliowaacha kwa chuki wainuke dhidi yako; nitawaleta wakushambulie kutoka pande zote. Nitawachochea Wababuloni na Wakaldayo wote, watu toka Pekodi, Shoa na Koa, pamoja na Waashuru wote. Nitawachochea vijana wote wa kuvutia, wakuu wa mikoa, makamanda, maofisa na wanajeshi wote wakiwa wapandafarasi. Watakujia kutoka kaskazini, pamoja na magari ya vita na ya mizigo, wakiongoza kundi kubwa la watu. Watakuzingira pande zote kwa ngao kubwa na ndogo na kofia za chuma. Nimewapa uwezo wa kukuhukumu, nao watakuhukumu kadiri ya sheria zao. Nami nitakuelekezea ghadhabu yangu, nao watakutenda kwa hasira kali. Watakukata pua na masikio na watu wako watakaosalia watauawa kwa upanga. Watawachukua watoto wako wa kiume na wa kike, na watu wako watakaosalia watateketezwa kwa moto. Watakuvua mavazi yako na kukunyanganya johari zako nzuri. Nitaukomesha uasherati na uzinzi wako ulioufanya tangu ulipokuwa kule Misri. Hutaziangalia sanamu zozote tena wala kuifikiria tena nchi ya Misri. “Naam, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitakutia mikononi mwa watu unaowachukia, watu unaowaona kuwa kinyaa. Na, kwa vile wanakuchukia, watakunyanganya matunda yote ya kazi yako na kukuacha uchi, bila nguo na kuonesha aibu ya uzinzi wako. Uzinzi wako na uasherati wako ndivyo vilivyokuletea hali hiyo. Wewe ulizini na mataifa, ukajitia najisi kwa miungu yao. Kwa kuwa ulifuata nyayo za dada yako, basi, mimi nitakupa kikombe kilekile cha adhabu ukinywe. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Utakunywa toka kikombe cha dada yako; kikombe kikubwa na cha kina kirefu. Watu watakucheka na kukudharau; na kikombe chenyewe kimejaa. Kitakulewesha na kukuhuzunisha sana. Kikombe cha dada yako Samaria, ni kikombe cha hofu na maangamizi. Utakinywa na kukimaliza kabisa; utakipasua vipandevipande kwa meno, na kurarua navyo matiti yako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa kuwa umenisahau na kunipa kisogo, basi, utawajibika kwa uasherati na uzinzi wako.” Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Wewe mtu! Je, uko tayari kuwahukumu Ohola na Oholiba? Basi, watangazie matendo yao ya kuchukiza! Wamefanya uzinzi na mauaji. Wamefanya ukahaba kwa sanamu zao, hata kuzitambikia watoto walionizalia wao wenyewe. Tena si hayo tu! Wameikufuru maskani yangu na kuzitangua sabato zangu. Siku ileile walipozitambikia sanamu watoto wao wenyewe, waliingia patakatifu ili wapatie unajisi. Hayo ndiyo waliyoyafanya nyumbani mwangu. “Hata walituma wajumbe wawaite watu wa mbali, nao wakaja. Kwa ajili yao, walioga, wakajitia wanja na kujipamba kwa johari. Kisha wakawa wameketi kwenye makochi mazurimazuri, na mbele yao meza imetandikwa. Juu ya meza hiyo waliweka ubani wangu na mafuta yangu. Basi, kukasikika sauti za kundi la watu wasiojali kitu, kundi la wanaume walevi walioletwa kutoka jangwani. Waliwavisha hao wanawake bangili mikononi mwao na taji nzuri vichwani mwao. Ndipo nikasema: Wanazini na mwanamke aliyechakaa kwa uzinzi. Kila mmoja alimwendea kama wanaume wamwendeavyo malaya. Ndivyo walivyowaendea Ohola na Oholiba wale wanawake waasherati. Lakini waamuzi waadilifu watawahukumu jinsi wanavyohukumu wazinzi na wauaji; kwa maana ni wazinzi na wauaji. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Genge la watu litaletwa, litawatisha na kuwapora mali zao. Genge hilo la watu litawapiga mawe, litawashambulia kwa upanga na kuwaua wana wao na binti zao, na nyumba zao wataziteketeza kwa moto. Ndivyo nitakavyokomesha uasherati wao katika nchi nzima, liwe onyo kwa wanawake wote wasifanye uzinzi kama huo mlioufanya. Na nyinyi Ohola na Oholiba, mtaadhibiwa kutokana na uzinzi wenu na dhambi yenu ya kuziabudu sanamu za miungu. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu.” Mnamo siku ya kumi, mwezi wa kumi, mwaka wa tisa tangu kuhamishwa kwetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Andika tarehe ya siku ya leo, maana hii ni siku ambapo mfalme wa Babuloni anaanza kuuzingira mji wa Yerusalemu. Wape mfano hao watu wangu waasi na kuwaambia kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Kiweke chungu juu ya meko, ukakijaze maji pia. Tia humo vipande vya nyama, vipande vizuri vya mapaja na mabega. Kijaze pia mifupa mizuri. Tumia nyama nzuri ya kondoo, panga kuni chini ya chungu, chemsha vipande vya nyama na mifupa, vyote uvichemshe vizuri. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wake mji wa mauaji! Mji huo ni kama chungu chenye kutu, ambacho kutu yake haiwezi kutoka! Vipande vya nyama ndani yake hutolewa kimojakimoja bila kuchaguliwa. Mauaji yamo humo mjini; damu yenyewe haikumwagwa udongoni ifunikwe na vumbi, ila ilimwagwa mwambani. Damu hiyo nimeiacha huko mwambani ili isifunikwe, nipate kuamsha ghadhabu yangu na kulipiza kisasi. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wake mji wa mauaji! Mimi nitarundika rundo kubwa la kuni. Nitaleta magogo ya kuni na kuwasha moto. Nitachemsha nyama vizuri sana. Nitachemsha na kukausha mchuzi, na mifupa nitaiunguza! Hicho chungu kitupu nitakiweka juu ya makaa kipate moto sana, shaba yake ipate moto, uchafu wake uyeyushwe na kutu iunguzwe. Lakini najisumbua bure; kutu yake nene haitoki hata kwa moto. Ewe Yerusalemu, matendo yako machafu yamekutia unajisi. Ingawa nilijaribu kuutakasa, wenyewe ulibaki najisi. Basi, hutatakasika tena mpaka nitakapoitosheleza hasira yangu juu yako. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Jambo hilo litakamilika; mimi nitalitenda. Sitaghairi jambo hilo wala kukuonea huruma. Nitakuadhibu kulingana na mwenendo na matendo yako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Tazama, kwa pigo moja nitakuondolea mpenzi wako. Lakini usiomboleze, wala kulia, wala kutoa machozi. Utasononeka, lakini sio kwa sauti. Hutamfanyia matanga huyo aliyekufa. Vaa viatu vyako na kuvaa kilemba; usiufunike uso wako wala kula chakula cha matanga.” Basi, asubuhi nilizungumza na watu, na jioni mke wangu akafariki. Na kesho yake asubuhi, nilifanya kama nilivyoamriwa. Watu wakaniuliza: “Je, jambo hili unalofanya lamaanisha nini kwetu?” Nikawajibu, “Mwenyezi-Mungu aliniagiza niwaambie nyinyi Waisraeli kwamba Mwenyezi-Mungu ataitia unajisi maskani yake, hiyo nyumba ambayo ni fahari ya ukuu wenu, na ambayo mnafurahi sana kuiona. Nao watoto wenu, wa kiume kwa wa kike, mliowaacha nyuma watauawa kwa upanga. Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya. Hamtazifunika nyuso zenu wala kula chakula cha matanga. Mtavaa vilemba vyenu na viatu miguuni; hamtaomboleza, wala kulia. Kutokana na maovu yenu, mtadhoofika na kusononeka, kila mtu na mwenzake. Nami Ezekieli nitakuwa ishara kwenu: Mtafanya kila kitu kama nilivyotenda. Wakati mambo hayo yatakapotukia, mtatambua kuwa yeye ndiye Bwana Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Wewe mtu! Siku ile nitakapoondoa kwao hicho ambacho ni tegemeo lao, na sababu ya shangwe yao, mahali ambapo wanapenda sana kupaona, nitawaondoa watoto wao wa kiume na wa kike. Siku hiyo, mtu atakayeokoka atakuja kukupasha habari hizo. Siku hiyohiyo, utaacha kuwa bubu, nawe utaweza kuongea naye. Kwa hiyo wewe utakuwa ishara kwao, nao watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Wageukie Waamoni, ukatoe unabii dhidi yao. Waambie Waamoni: Sikilizeni neno la Bwana Mwenyezi-Mungu: Nyinyi mlifurahia kuona maskani yangu ikitiwa unajisi, nchi ya Israeli ikiangamizwa na watu wa Yuda wakipelekwa uhamishoni. Basi, nitawatia nyinyi mikononi mwa watu wa mashariki; watapiga hema zao kati yenu na kufanya makazi yao katika nchi yenu. Nao watakula matunda yenu na kunywa maziwa yenu. Mji wa Raba nitaufanya kuwa malisho ya ngamia na nchi ya Amoni zizi la kondoo. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa sababu mlipiga makofi, mkarukaruka kwa furaha na kushangilia sana juu ya nchi ya Israeli, basi, mimi nimeunyosha mkono dhidi yenu; nitawaacha mtekwe nyara na watu wa mataifa mengine. Nitawaangamizeni, nanyi hamtakuwa taifa tena wala kuwa na nchi. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Bwana Mwenyezi-Mungu alisema: “Kwa kuwa Moabu imesema kuwa Yuda ni sawa tu na mataifa mengine, mimi nitaifanya miji inayolinda mipaka ya Moabu ishambuliwe, hata miji ile bora kabisa, yaani Beth-yeshimothi, Baal-meoni na Kiriathaimu. Nitaitia nchi hiyo pamoja na nchi ya Amoni mikononi mwa watu wa mashariki iwe mali yao. Nchi ya Moabu haitakuwa taifa tena. Mimi nitaiadhibu nchi ya Moabu, nao watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Bwana Mwenyezi-Mungu alisema hivi: “Kwa kuwa Waedomu wamefanya kisasi na Yuda, wakawalipiza watu wa Yuda kisasi kibaya sana basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitanyosha mkono dhidi ya nchi ya Edomu na kuwaua watu wote na wanyama. Nitaifanya kuwa ukiwa kutoka mji wa Temani hadi mji wa Dedani, watu watauawa kwa upanga. Nitawafanya watu wangu Israeli walipize kisasi juu ya Waedomu nao watawatenda Waedomu kadiri ya hasira na ghadhabu yangu. Ndipo Waedomu watakapotambua uzito wa kisasi changu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nimesema.” Bwana Mwenyezi-Mungu alisema hivi: “Kwa kuwa Wafilisti walifanya kisasi, wakawalipiza kisasi adui zao kwa ubaya sana na kuendelea kuwa maadui zao daima, basi, mimi Mwenyezi-Mungu nitanyosha mkono dhidi ya Wafilisti; nitawaangamiza hao Wakerethi na wakazi wa pwani. Nitawalipiza kisasi kikali kwa adhabu ya ghadhabu. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Mnamo siku ya kwanza ya mwezi, mwaka wa kumi na moja tangu kuhamishwa kwetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Watu wa Tiro wameucheka mji wa Yerusalemu na kusema: ‘Aha! Yerusalemu mji ambao watu wote walipita, umeangamizwa! Sasa umetuachia nafasi; utajiri wake umeharibiwa!’ Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Sasa nitapambana nawe ewe Tiro. Nitazusha mataifa mengi dhidi yako, nao watakuja kama mawimbi ya bahari. Wataziharibu kuta zako na kuibomoa minara yako. Nitafagilia mbali udongo wako na kukufanya kuwa jabali tupu. Utakuwa mahali pakavu katikati ya bahari, na wavuvi watakausha nyavu zao hapo; mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mataifa yatakuteka nyara, na miji iliyo jirani nawe huko bara itaangamizwa. Nao watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kutoka kaskazini nitamleta Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, mfalme wa wafalme, akiwa na farasi, magari ya vita, wapandafarasi na jeshi kubwa, aje kukushambulia. Ataiangamiza miji iliyo jirani nawe huko bara. Kisha atajenga kuta za kukushambulia, atajaza udongo kwenye kuta zako na kuweka ukuta wenye ngao ili kukushambulia. Ataweka magogo yake ya kubomolea mbele ya kuta zako, na kwa mitalimbo ataivunjilia mbali minara yako. Farasi wa mfalme Nebukadneza ni wengi na vumbi watakalotimua litakufunika. Kuta zako zitatetemeka kwa mshindo wa wapandafarasi na magari ya vita na ya mizigo wakati atakapoingia kwenye malango yako kama watu waingiavyo mjini kupitia mahali palipobomolewa. Kwa kwato za farasi wake, ataikanyaga mitaa yako yote. Atawaua watu wako kwa panga; minara yako mikubwa ataiangusha chini. Utajiri wako watauteka pamoja na bidhaa zako. Watazibomoa kuta zako na kuziangusha nyumba zako za fahari; mawe, mbao na udongo ulivyotumia kujengea nyumba hizo watavitupa baharini. Nitakomesha muziki wa nyimbo zako. Sauti za vinubi vyako hazitasikika tena. Nitakufanya kuwa jabali tupu; utakuwa mahali pa wavuvi kukaushia nyavu zao, wala hutajengwa tena. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia hivi wewe Tiro: Wakazi wa sehemu za pwani watatetemeka watakaposikia kishindo cha kuanguka kwako na mlio wa majeruhi na wa watu wanaouawa. Wakuu wote wa mataifa ya pwani watashuka toka viti vyao vya enzi, na kuvua mavazi yao ya heshima pamoja na nguo zao zilizotariziwa. Wakiwa wamejaa hofu, wataketi chini; nao watatetemeka wakati wote na kushangaa mno juu ya hayo yaliyokupata. Wataimba utenzi huu wa kuomboleza: Umeangamizwa wewe mji maarufu, umetoweka kutoka baharini! Wakazi wake walieneza nguvu zao juu ya bahari, ambapo walihofiwa na wote. Sasa watu wa bara wanatetemeka kwa sababu ya kuanguka kwake; wakazi wa pwani, wametishika kwa kutoweka kwako! “Maana, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitakufanya wewe Tiro kuwa mahame, kama miji isiyo na watu, nitakapoleta juu yako maji kutoka vilindi vya bahari, na maji mengi yatakufunika. Nitakuteremsha shimoni ili ujiunge na walioko huko, walioishi duniani zamani; nitakufanya ukae huko katika mahame milele. Hutakaliwa na watu milele na hutakuwa na nafasi miongoni mwa nchi za walio hai. Nitakufanya kuwa kitisho wala hutakuwapo tena; watu watakutafuta, lakini hawatakupata tena. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Sasa ewe mtu, imba utenzi huu wa maombolezo juu ya mji wa Tiro, mji ule kando ya bahari, unaofanya biashara na mataifa ya pwani. Uambie: Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: Ewe Tiro, wewe umejigamba u mzuri kwelikweli! Mipaka yako imeenea kwelikweli! Umejengwa kama meli nzuri. Wajenzi wako walitumia misonobari kutoka Seniri kupasua mbao zako zote; walichukua mierezi kutoka Lebanoni kukutengenezea mlingoti. Walichukua mialoni toka Bashani wakakuchongea makasia yako; walikitengenezea silaha kwa misonobari ya kisiwa cha Kupro, na kuipamba kwa pembe. Kitani kilichotariziwa kutoka Misri kilikuwa kwa kupamba tanga lako na kwa ajili ya bendera yako. Chandarua chako kilitengenezwa kwa rangi ya samawati na urujuani kutoka visiwa vya Elisha. Watu wa Sidoni na Arvadi walikuwa wapiga makasia wako. Wenye hekima wako walikuwa ndani wakifanya kazi kama wanamaji. Wazee wa Gebali na mafundi wao walikuwa kwako kuziba nyufa zako. Mabaharia waliokuwa wakipitia kwako walifanya biashara nawe. Watu kutoka Persia, Ludi na Puti walijiunga katika jeshi lako; walirundika kwenye kambi zao za jeshi ngao zao na kofia zao. Wanajeshi hao walikupatia fahari. Watu wa Arvadi na wa Hele na jeshi lao walilinda kuta zako pande zote, nao watu wa Gamadi walilinda minara yako. Walitundika ngao zao kwenye kuta zako pande zote, na hivyo wakaukamilisha uzuri wako. Watu wa Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mwingi na wa kila namna. Walitoa fedha, chuma, bati, na risasi kupata bidhaa zako. Watu wa Yavani, Tubali na Mesheki, walifanya biashara nawe, wakakupatia watumwa na vifaa vya shaba wapate bidhaa zako. Bidhaa zako uliziuza huko Beth-togarma ili kujipatia farasi wa mizigo na wa vita, ngamia na nyumbu. Watu wa Dedani walifanya biashara nawe. Nchi nyingi za pwani zilikuwa masoko yako maalumu. Watu wake walikuletea pembe za ndovu na mipingo kulipia bidhaa zako. Watu wa Edomu walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako. Kwa kupata bidhaa zako walikupa akiki, vitambaa vya urujuani, vitambaa vilivyonakshiwa, kitani safi, matumbawe na yakuti. Hata watu wa Yuda na Israeli walifanya biashara nawe; walikupa ngano, zeituni, tini za mwanzoni, asali, mafuta na marhamu kulipia bidhaa zako. Watu wa Damasko walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako; walikupa divai kutoka Helboni na sufu nyeupe. Vedani na Yavani walisafirisha bidhaa zako toka Uzali; hata chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai ili kupata bidhaa zako. Watu wa Dedani walifanya biashara nawe kwa kukupatia matandiko ya farasi. Waarabu na wakuu wote wa nchi ya Kedari walikuwa wachuuzi wako wakuu katika biashara ya wanakondoo, kondoo madume na mbuzi. Wachuuzi wa Sheba na wa Rama walifanya biashara nawe; walikuletea viungo vya chakula, vito vya thamani na dhahabu kujipatia bidhaa zako safi. Wakazi wa miji ya Harani, Kane na Edeni na wachuuzi wa Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe. Hao walifanya nawe biashara ya mavazi ya fahari, nguo za buluu zilizotariziwa, mazulia ya rangi angavu vifundo na kamba zilizosokotwa imara. Merikebu za Tarshishi ndizo zilikusafirishia bidhaa zako. Basi kama meli katikati ya bahari wewe ulikuwa umejaa shehena. Wapiga makasia wako walikupeleka mbali baharini. Upepo wa mashariki umekuvunjavunja ukiwa mbali katikati ya bahari. Utajiri wako wa bidhaa na mali, wanamaji wako wote chomboni, mafundi wako wa meli na wachuuzi wako, askari wako wote walioko kwako, pamoja na wasafiri walioko kwako, wote wataangamia baharini, siku ile ya kuangamizwa kwako. Mlio wa mabaharia wako utakaposikika, nchi za pwani zitatetemeka. Hapo wapiga makasia wote wataziacha meli zao. Wanamaji na manahodha watakaa pwani. Wataomboleza kwa uchungu wa moyo juu yako, na kulia kwa uchungu mkubwa; watajitupia mavumbi vichwani mwao na kugaagaa kwenye majivu. Wamejinyoa vichwa kwa ajili yako na kuvaa mavazi ya gunia. Watalia kwa uchungu wa moyo juu yako. Wataimba wimbo wa ombolezo juu yako; ‘Nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro katikati ya bahari?’ Bidhaa zako zilipowasili nchi za ngambo, ulitosheleza mahitaji ya watu wengi! Kwa wingi wa utajiri wa bidhaa zako uliwatajirisha wafalme wa dunia. Lakini sasa umevunjikia baharini; umeangamia katika vilindi vya maji. Shehena yako na jamii ya mabaharia vimezama pamoja nawe. Wakazi wote wa visiwani wamepigwa na bumbuazi juu yako; wafalme wao wameogopa kupindukia, nyuso zimekunjamana kwa huzuni. Wachuuzi wa mataifa watakufyonya! Umeufikia mwisho wa kutisha, na hutakuwapo tena milele!” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Mwambie mfalme wa Tiro kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe una kiburi cha moyo, na umesema kwamba wewe ni mungu, kwamba umekalia kiti cha enzi cha miungu, umekaa mbali huko baharini. Lakini, wewe ni binadamu tu wala si Mungu, ingawa wajiona kuwa una hekima kama Mungu. Haya! Wewe wajiona mwenye hekima kuliko Danieli, wadhani hakuna siri yoyote usiyoijua. Kwa hekima na akili yako umejipatia utajiri, umejikusanyia dhahabu na fedha ukaziweka katika hazina zako. Kwa busara yako kubwa katika biashara umejiongezea utajiri wako, ukawa na kiburi kwa mali zako! Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa vile unajiona mwenye hekima kama Mungu, basi nitakuletea watu wageni, mataifa katili kuliko yote. Wataharibu fahari ya hekima yako na kuchafua uzuri wako. Watakutumbukiza chini shimoni, nawe utakufa kifo cha kikatili kilindini mwa bahari. Je, utajiona bado kuwa mungu mbele ya hao watakaokuua? Mikononi mwa hao watakaokuangamiza, utatambua kuwa wewe ni mtu tu, wala si Mungu! Utakufa kifo cha aibu kubwa mikononi mwa watu wa mataifa. Ni mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Tena neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Imba wimbo wa maombolezo juu ya mfalme wa Tiro. Mwambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe mfalme wa Tiro ulikuwa upeo wa ukamilifu; ulijaa hekima na uzuri kamili. Ulikaa Edeni, bustani ya Mungu. Ulipambwa kwa kila namna ya johari, akiki, topazi, yaspi, zabarajadi, berili, sardoniki, johari ya rangi ya samawati, almasi na zumaridi. Ulikuwa na mapambo ya dhahabu. Yote uliwekewa tayari siku ulipoumbwa. Nilimteua malaika kukulinda, uliishi katika mlima wangu mtakatifu na kutembea juu ya vito vinavyometameta. Uliishi maisha yasiyo na lawama, tangu siku ile ulipoumbwa, hadi ulipoanza kufanya uovu. Ufanisi wa biashara yako ulikujaza dhuluma, ukatenda dhambi. Kwa hiyo nilikufukuza kama kinyaa, mbali na mlima wangu mtakatifu. Na yule malaika aliyekulinda akakufukuzia mbali na vito vinavyometameta. Ulikuwa na kiburi kwa sababu ya uzuri wako. Uliharibu hekima yako kwa sababu ya fahari yako. Nilikubwaga chini udongoni, nikakufanya kuwa kioja kwa wafalme. Kwa wingi wa uhalifu wako na udanganyifu katika biashara yako ulipachafua mahali pako pa ibada; kwa hiyo nilizusha moto kwako, nao ukakuteketeza, nami nikakufanya majivu juu ya nchi, mbele ya wote waliokutazama. Wote wanaokufahamu kati ya mataifa wameshikwa na mshangao juu yako. Umeufikia mwisho wa kutisha, na hutakuwapo tena milele.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Ugeukie mji wa Sidoni, utoe unabii juu yake kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi nitapambana nawe Sidoni, na kuudhihirisha utukufu wangu kati yako. Nitakapotekeleza hukumu zangu juu yako na kukudhihirishia utakatifu wangu, ndipo utakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nitakupelekea maradhi mabaya na umwagaji damu utafanyika katika barabara zako. Utashambuliwa kwa upanga toka pande zote na watu wako watakaouawa, watakuwa wengi. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Mungu asema, “Mataifa jirani na Waisraeli ambayo yalikuwa yanawaudhi hayataweza tena kuwaumiza Waisraeli kama vile kwa miiba na michongoma. Ndipo watakapojua ya kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawakusanya na kuwaleta Waisraeli kutoka katika mataifa yote ambamo walitawanywa. Hivyo nitawafanya watu wa mataifa waone kuwa mimi ni mtakatifu. Watu wa Israeli wataishi katika nchi yao ambayo mimi nilimpa mtumishi wangu Yakobo. Watakaa humo salama salimini; watajenga nyumba na kupanda mizabibu. Wataishi bila hofu maana mataifa jirani zao ambayo yaliwaudhi, mimi nitayaadhibu. Hapo watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.” Siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kumi, mwaka wa kumi tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Mgeukie Farao mfalme wa Misri, utoe unabii juu yake na nchi yote ya Misri. Mwambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi nitapambana na wewe mfalme wa Misri, wewe mamba ulalaye mtoni Nili! Wewe unafikiri kwamba Nili ni wako, kwamba wewe ndiwe uliyeufanya! Basi, nitakutia ndoana tayani mwako, na kufanya samaki wakwame magambani mwako. Nitakuvua kutoka huko mtoni. Nitakutupa jangwani, wewe na samaki hao wote. Mwili wako utaanguka mbugani; wala hakuna atakayekuokota akuzike. Nimeutoa mwili wako uwe chakula cha wanyama wakali na ndege. Hapo ndipo wakazi wote wa Misri watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Waisraeli walikutegemea wewe ee Misri, lakini umekuwa dhaifu kama utete. Walipokushika kwa mkono, ulivunjika na kutegua mabega yao. Walipokuegemea ulivunjika na kutetemesha viungo vyao. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitazusha upanga dhidi yako na kuwaua watu na wanyama wako wote. Kwa sababu umesema kuwa mto Nili ni wako, kwamba ndiwe uliyeufanya, basi, nchi yako, Misri, itakuwa tupu na jangwa. Ndipo watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Hakika nitakuadhibu wewe na mito yako; kwa hiyo nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa na tupu toka Migdoli mpaka Syene hadi mipakani mwa Kushi. Hakuna mtu wala mnyama atakayepita huko. Haitakaliwa kwa muda wa miaka arubaini. Kati ya miji yote iliyoharibiwa, miji ya Misri itakuwa mitupu kwa miaka arubaini. Nitawatawanya Wamisri kati ya watu wa mataifa mengine na kuwasambaza katika nchi nyingine. “Lakini mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Baada ya miaka arubaini nitawakusanya Wamisri kutoka kwa mataifa walimotawanywa. Nitawafanikisha tena Wamisri. Nitawarudisha katika nchi ya Pathrosi, nchi yao ya asili. Huko watakuwa na ufalme usio na nguvu, ufalme dhaifu kuliko falme zote; wala hawataweza kujikuza juu ya mataifa mengine. Nitawafanya Wamisri wawe watu dhaifu hata wasiweze kuyatawala mataifa mengine tena. Misri haitakuwa tena na nguvu za kuweza kutegemewa na watu wa Israeli. Waisraeli watakumbuka jinsi walivyokosa kwa kutegemea nchi ya Misri. Waisraeli watatambua kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu.” Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, mwaka wa ishirini na saba tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, alilipa jeshi lake jukumu gumu la kuishambulia Tiro. Vichwa vyote vya wanajeshi wake vilipata upara na mabega yote yalichubuka. Lakini yeye, wala jeshi lake, hawakuambulia chochote kutokana na uvamizi huo alioufanya dhidi ya Tiro. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitampa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, nchi ya Misri. Ataipora mali yake yote, na kuchukua utajiri wa Misri kuwa ujira wa jeshi lake. Nimempa nchi ya Misri kuwa ujira wa jasho lake kwa kuwa majeshi yake yalifanya kazi kwa ajili yangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Siku hiyo, nitawafanya Waisraeli wawe na nguvu na kukuwezesha wewe Ezekieli uongee miongoni mwao. Nao watapata kujua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Toa unabii useme kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ombolezeni na kusema: ‘Ole wetu siku ile!’ Kwa maana, siku hiyo imekaribia; siku ile ya Mwenyezi-Mungu iko karibu. Hiyo itakuwa siku ya mawingu, siku ya maangamizi kwa mataifa. Vita vitazuka dhidi ya Misri, na wasiwasi mkuu utaikumba nchi ya Kushi, wakati Wamisri wengi wataanguka wameuawa, mali zao zitakapochukuliwa, na misingi ya miji yao kubomolewa. “Watu wote waliofungamana na Wamisri, yaani watu wa Kushi, Puti, Ludi, Arabia yote na Libia wataangamia pamoja nao. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wote wanaoiunga mkono Misri wataangamia, mashujaa wake wenye fahari wataangamizwa, tangu Migdoli mpaka Syene watu watauawa vitani. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Misri itakuwa jangwa kama nchi zilizo jangwa na miji yake itakuwa magofu kama miji iliyoteketezwa. Nitakapoiteketeza Misri kwa moto na kuwavunjilia mbali wasaidizi wake wote ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Siku hiyo, nitapeleka wajumbe kwenda kuwatisha Waethiopia wanaojidhani kuwa salama. Watatetemeka siku Misri itakapoangamia. Naam! Kweli siku hiyo yaja! “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitamtumia Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, kukomesha utajiri wa nchi ya Misri. Nebukadneza mwenyewe pamoja na watu wake, taifa katili kuliko mataifa yote, watatumwa kuiangamiza nchi ya Misri. Watachomoa panga zao dhidi ya Misri na kuijaza nchi hiyo watu waliouawa. Nitaukausha mto Nili na vijito vyake, na kuwauzia watu waovu nchi ya Misri. Nitasababisha uharibifu nchini kote kwa mkono wa watu wageni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitaharibu vinyago vya miungu, na kukomesha sanamu mjini Memfisi. Hakutakuwa na mkuu tena huko Misri. Nitasababisha hofu itawale nchini Misri. Mji wa Pathrosi nitaufanya kuwa mtupu, mji wa Soani nitauwasha moto, mji wa Thebesi nitauadhibu. Nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Pelusiumu, ile ngome inayotegemewa na Misri; na kuangamiza makundi ya Thebesi. Nitaiwasha moto nchi ya Misri. Pelusiumu utashikwa na dhiki kubwa, ukuta wa Thebesi utabomolewa, nao Memfisi utakabiliwa na adui mchana wazi. Vijana wanaume wa Oni na Pi-besethi watauawa kwa upanga, na wakazi wengine watachukuliwa uhamishoni. Huko Tahpanesi mchana utakuwa giza wakati nitavunja mamlaka ya Misri na kiburi chake kikuu kukomeshwa. Wingu litaifunika nchi ya Misri na watu wake watachukuliwa mateka. Ndivyo nitakavyoiadhibu Misri. Na watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Siku ya saba ya mwezi wa kwanza, mwaka wa kumi na moja tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Nimeuvunja mkono wa Farao mfalme wa Misri, nao haukufungwa ili uweze kupona na kuweza kushika upanga. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitapambana na Farao mfalme wa Misri. Nitaivunja mikono yake yote miwili, ule mzima na hata uliovunjika. Na upanga ulio mkononi mwake utaanguka chini. Nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa na kuwasambaza katika nchi nyingine. Mikono ya mfalme wa Babuloni nitaitia nguvu na kutia upanga wangu mkononi mwake. Lakini nitaivunja mikono ya Farao, naye atapiga kite mbele ya mfalme wa Babuloni kama mtu aliyejeruhiwa vibaya sana. Mikono ya mfalme wa Babuloni nitaiimarisha, lakini mikono ya Farao italegea. Hapo watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nitakapotia upanga wangu mkononi mwa mfalme wa Babuloni, ataunyosha dhidi ya nchi ya Misri, nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa mengine na kuwasambaza katika nchi nyingine. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa tatu, mwaka wa kumi na moja tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Mwambie hivi Farao mfalme wa Misri na watu wake wote: Wewe wafanana na nini kwa ukuu wako? Wewe ni kama mwerezi wa Lebanoni wenye matawi mazuri na majani mengi na shina refu. Kilele chake kinafika hata mawinguni. Maji yaliustawisha, vilindi vya maji viliulisha. Mito ilibubujika mahali ulipoota, ikapeleka vijito kwenye miti yote ya msituni. “Kwa hiyo, ulirefuka sana kupita miti yote msituni; matawi yake yalizidi kuwa mengi na makubwa, kutokana na maji mengi mizizini mwake. Ndege wote waliweka viota matawini mwake, chini yake wanyama walizaliwa, mataifa yote makubwa yaliburudika kivulini mwake. Ulikuwa mzuri kwa ukubwa wake, na kwa urefu wa matawi yake. Mizizi yake ilipenya chini mpaka penye maji mengi. Miongoni mwa mierezi ya bustanini mwa Mungu, hakuna mti uliolingana nao, wala misonobari haikulingana na matawi yake, mibambakofi haikuwa na matawi kama yake, hata mti wowote wa bustani ya Mungu haukulingana nao kwa uzuri. Mimi niliufanya kuwa mzuri kwa matawi yake mengi; ulionewa wivu na miti yote ya Edeni iliyokuwa katika bustani ya Mungu. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa sababu wewe ulirefusha kimo chake na kukiinua kilele chake kati ya matawi makubwa, ukajivunia urefu wake, nitautia mikononi mwa mkuu kati ya mataifa. Yeye, atauadhibu. Nimeutupilia mbali kadiri ya uovu wake. Watu wa mataifa mengine katili kupindukia, wataukata na kuubwaga chini na kuuacha. Matawi yake yataanguka chini mlimani na kila mahali mabondeni; yatavunjika na kutapakaa chini katika magenge yote. Watu wote wataondoka kivulini mwake na kuuacha. Ndege wote watatua juu ya mabaki yake na wanyama wote wa porini watakanyaga matawi yake. Hayo yameupata ili mti wowote ulio mahali penye maji usiweze kurefuka tena kiasi hicho wala kukifikisha kilele chake mawinguni. Mti wowote unaonyweshwa maji usiweze tena kufikia urefu huo. Kwa maana kila kitu mwisho wake ni kifo; hali kadhalika na watu. Wote watashiriki hali yao washukao shimoni kwa wafu. “Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ileile mwerezi ulipofika kuzimu nilitandaza giza nene juu yake nikaufunika; mito yake niliikausha na mtiririko wa maji yake mengi nikaukomesha. Nayo Lebanoni niliiweka gizani kwa ajili yake, na miti yote msituni ikazirai kwa ajili yake. Niliyafanya mataifa yatetemeke kwa sauti ya kuanguka kwake, naam, wakati nilipouangusha chini kuzimu pamoja nao washukao shimoni kwa wafu nayo miti yote ya Edeni, miti mizuri na ya pekee ya Lebanoni ambayo ilimwagiliwa maji ilifarijiwa huko chini kwa wafu. Hiyo nayo ilishuka huko kuzimu pamoja nao, ikajiunga na wale waliofungamana nao na ambao waliburudika chini ya kivuli chake. “Kwa uzuri na ukuu wa mti huo, hamna mti wowote bustanini Edeni ambao uliweza kulinganishwa nao. Sasa, mti huo ni wewe mfalme Farao. Wewe utatupwa chini kwa wafu pamoja na miti ya Edeni. Utalala karibu na wale wasiomjua Mungu na wale waliouawa kwa upanga. Hiyo itakuwa hali yako ewe Farao, wewe na watu wako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na mbili, mwaka wa kumi na mbili tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Imba utenzi wa kuomboleza juu ya Farao, mfalme wa Misri. Wewe Farao unajiona kuwa simba kati ya mataifa, lakini wewe ni kama mamba tu majini: Unachomoka kwa nguvu kwenye mito yako, wayavuruga maji kwa miguu yako, na kuichafua mito. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitautupa wavu wangu juu yako, nao watu watakuvua humo kwa wavu wangu. Nitakutupa juu ya nchi kavu, nitakubwaga uwanjani, nitawafanya ndege wote watue juu yako, na kuwashibisha wanyama wote wa porini kwa mwili wako. Nitatawanya nyama yako milimani, na kujaza mabonde yote mzoga wako. Nchi nitainywesha damu yako mpaka milimani, mashimo yatajaa damu yako. Nitakapokuangamiza, nitazifunika mbingu, nitazifanya nyota kuwa nyeusi, jua nitalifunika kwa mawingu, na mwezi hautatoa mwangaza wake. Nitaifanya mianga yote mbinguni kuwa giza, nitatandaza giza juu ya nchi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitaihuzunisha mioyo ya watu wengi, nitakapokupeleka utumwani kati ya mataifa, katika nchi ambazo huzijua. Nitayashtusha mataifa mengi kwa habari zako, wafalme wao watatetemeka kwa sababu yako, nitakaponyosha upanga wangu mbele yao. Watatetemeka kila wakati, kila mtu akihofia uhai wake, siku ile ya kuangamia kwako. Kwa maana, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Upanga wa mfalme wa Babuloni utakufuatia. Watu wako wengi watauawa kwa mapanga ya mashujaa, watu katili kuliko mataifa yote. Watakomesha kiburi cha Misri na kuwaua watu wako wote. Nitaiangamiza mifugo yako yote kando ya mto Nili. Maji yake hayatavurugwa tena na mtu wala kwato za mnyama kuyachafua tena. Hapo nitayafanya maji yake yatulie na kuitiririsha mito yake kama mafuta. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa jangwa na mali yake yote kuchukuliwa, nitakapowaua wakazi wake wote, ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Huo ndio utenzi wa maombolezo, wanawake wa mataifa watauimba, wataimba juu ya Misri na watu wake wote. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nimesema.” Siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza, mwaka wa kumi na mbili tangu kuhamishwa kwetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Waombolezee watu wengi wa Misri. Wapeleke chini kwenye nchi ya wafu pamoja na mataifa mengine yenye nguvu, waende huko pamoja nao washukao chini kwa wafu. Waambie: Nyinyi ni wazuri kuliko nani? Nendeni kuzimu mlazwe pamoja na wasiomjua Mungu! Watu wa Misri wataangamia pamoja na watu waliouawa vitani. Upanga uko tayari kuangamiza Misri pamoja na watu wake wengi. Wakuu wenye nguvu pamoja na wasaidizi wao wakiwa huko shimoni kwa wafu watasema hivi: ‘Wamisri wameshuka chini kwa wafu, wanalala pamoja na watu wasiomjua Mungu, waliouawa vitani.’ “Waashuru wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Wote waliuawa vitani, na makaburi yao yako sehemu za chini kabisa shimoni kwa wafu. Wanajeshi wao wote waliuawa vitani na makaburi yao yamewazunguka. Hapo awali, walipokuwa wanaishi bado, walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. “Waelamu pia wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao waliouawa vitani. Wote hao wasiomjua Mungu walishuka kwenye nchi ya wafu. Walipokuwa wanaishi bado walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. Lakini sasa wanabeba aibu yao pamoja na wanaoshuka shimoni kwa wafu. Wamelazwa na jeshi lao miongoni mwa wale waliouawa vitani. Wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wake wote waliouawa vitani na ambao wote hawamjui Mungu. Walipokuwa bado wanaishi walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai, na sasa wako hapo wamejaa aibu pamoja na wale waliouawa vitani. “Watu wa Mesheki na wa Tabali wote wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Watu hao wote wasiomjua Mungu walikufa vitani, watu ambao walipokuwa hai walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. Hao wasiomjua Mungu hawakuzikwa pamoja na mashujaa wa kale, ambao walikwenda kuzimu kwa wafu wakiwa na silaha zao, mapanga yao chini ya vichwa vyao na ngao zao juu ya miili yao. Mashujaa hao walipokuwa wanaishi bado walijaza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. Basi, nyinyi Wamisri mtaangamizwa na kulazwa miongoni mwa wasiomjua Mungu waliouawa vitani. “Waedomu wako huko pamoja na wafalme wao na wakuu wao wote. Walipokuwa bado hai walikuwa na nguvu sana, lakini sasa wamelazwa kwa wafu pamoja na wasiomjua Mungu waliouawa vitani. “Viongozi wote wa watu wa kaskazini wako huko pia; hata Wasidoni wote walikwenda kujiunga na wafu. Walipokuwa bado wanaishi, walisababisha vitisho kwa nguvu zao, lakini sasa hao wasiomjua Mungu wamelazwa chini kwa aibu pamoja na wale waliouawa vitani. Wanashiriki aibu ya wale walioshuka shimoni kwa wafu. “Farao, atakapowaona hao wote atafarijika kwa ajili ya wingi wa majeshi yake yote; mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Nilimfanya Farao aeneze vitisho katika nchi ya walio hai, lakini sasa yeye mwenyewe pamoja na jeshi lake lote watauawa vitani na kulazwa pamoja na wasiomjua Mungu, waliokufa vitani. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Ongea na wananchi wenzako, uwaambie hivi: Kama nikizusha vita katika nchi fulani, na watu wa nchi hiyo wakamchagua mmoja wao awe mlinzi wao, huyo anapoona maadui wanakuja, atapiga tarumbeta na kuwaonya watu. Mtu akisikia sauti ya tarumbeta lakini akapuuza onyo hilo, maadui wakaja na kumuua, yeye mwenyewe atawajibika kwa kifo chake. Aliisikia sauti ya tarumbeta, akapuuza onyo; basi lawama ya kifo chake itakuwa juu yake mwenyewe. Lakini kama angejali hilo onyo, angeyaokoa maisha yake. “Lakini kama yule mlinzi akiona adui wanakuja asipige tarumbeta na watu wakawa hawakuonywa juu ya hatari inayokuja, maadui wakaja na kumuua mtu yeyote miongoni mwao; huyo mtu aliyekufa, atakuwa amekufa kwa kosa lake. Lakini mimi nitamdai mlinzi kifo cha mtu huyo. “Basi, ewe mtu, nimekuweka kuwa mlinzi wa Waisraeli. Utakaposikia neno kutoka kwangu utawapa onyo langu. Nikimwambia mtu mwovu: ‘Wewe mtu mwovu hakika utakufa’; lakini wewe husemi chochote ili kumwonya yule mtu mwovu aachane na mwenendo wake; mtu huyo hakika atakufa kwa kosa lake; walakini nitakudai wewe kifo chake. Lakini ukimwonya mwovu aachane na mwenendo wake, naye haachani na mwenendo wake mbaya, yeye atakufa kwa kosa lake; lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako. “Ewe mtu! Waambie Waisraeli jambo hili: Nyinyi mwasema, ‘Tumezidiwa na makosa na dhambi zetu. Tunadhoofika kwa sababu yake! Tutawezaje basi, kuishi?’ Basi, waambie: Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu naapa kwamba, mimi sikifurahii kifo cha mtu mwovu, bali napenda mtu mwovu aachane na mwenendo wake mbaya, apate kuishi. Tubuni, achaneni na mwenendo wenu mbaya, enyi Waisraeli! Kwa nini mwataka kufa? “Basi, ewe mtu, waambie wananchi wenzako hivi: Mtu mwadilifu akitenda uovu, uadilifu wake hautamwokoa. Na mtu mwovu akiacha kutenda dhambi hataadhibiwa. Mtu mwadilifu akianza kutenda dhambi uadilifu wake hautamsalimisha. Mimi namwahidi mwadilifu kwamba ataishi; lakini yeye akiamini kwamba uadilifu wake watosha, akaanza kutenda uovu, matendo yake yote mema ya hapo awali hayatakumbukwa; atakufa kwa uovu wake. Tena, nikimwambia mtu mwovu kuwa hakika atakufa naye akaiacha dhambi yake, akaanza kutenda yaliyo ya haki na sawa, hatakufa; kama akirudisha rehani na kurudisha alichoiba, akafuata kanuni ziletazo uhai bila kutenda uovu, mtu huyo hakika ataishi; hatakufa. Dhambi zake zote alizotenda hapo awali hazitakumbukwa; yeye ametenda yaliyo ya haki na mema; kwa hiyo hakika ataishi. “Lakini wananchi wenzako wasema ati: ‘Anachofanya Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Kumbe kwa kweli wao ndio hawafanyi kilicho sawa. Mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake, akaanza kutenda uovu, atakufa kwa sababu ya uovu wake. Na mtu mwovu akiacha uovu wake, akaanza kutenda mambo ya haki na mema ataishi kwa sababu ya matendo yake mema. Lakini, nyinyi mwasema ati: ‘Anachofanya Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Enyi Waisraeli, mimi nitamhukumu kila mmoja wenu kadiri ya matendo yake.” Siku ya tano ya mwezi wa kumi, mwaka wa kumi na mbili wa uhamisho wetu, mtu mmoja aliyetoroka kutoka Yerusalemu alinijia, akasema: “Mji wa Yerusalemu umetekwa!” Wakati alipofika huyo mtu ilikuwa asubuhi kumbe jana yake jioni mimi nilisikia uzito wa nguvu yake Mwenyezi-Mungu. Basi, huyo mkimbizi alipowasili kwangu kesho yake asubuhi, nikaacha kuwa bubu, nikaanza kuongea tena. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Wakazi waliobaki katika miji iliyoharibiwa nchini Israeli wanasema, ‘Abrahamu alikuwa peke yake, hata hivyo, alipata kuimiliki nchi hii. Lakini sisi ni wengi; ni dhahiri tumepewa nchi hii iwe yetu!’ Basi, waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nyinyi mnakula nyama yenye damu, mnaziabudu sanamu za miungu yenu na kuua! Je, mnadhani mtapewa nchi hii iwe yenu? Mnategemea silaha zenu, mnafanya mambo ya kuchukiza na kila mwanamume miongoni mwenu anatembea na mke wa jirani yake! Je, mnadhani mtapewa nchi hii iwe yenu? Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kama niishivyo mimi naapa kwamba hao wanaokaa katika miji hiyo iliyo magofu, wataangamia kwa upanga; aliye uwanjani nitamtoa aliwe na wanyama wakali; na wale walio ndani ya ngome na mapangoni watakufa kwa maradhi mabaya. Nitaifanya nchi kuwa jangwa na tupu. Mashujaa wake wenye kiburi nitawaua. Milima ya Israeli itakuwa jangwa na hakuna mtu atakayepita huko. Naam, nitakapoifanya hiyo nchi kuwa jangwa na tupu kwa sababu ya mambo yote ya kuchukiza waliyotenda, ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Wewe mtu! Wananchi wenzako wanazungumza juu yako, wameketi kutani na milangoni mwa nyumba zao na kuambiana: ‘Haya! Twende tukasikie neno alilosema Mwenyezi-Mungu!’ Basi, hukujia makundi kwa makundi na kuketi mbele yako kama watu wangu, wasikie unachosema, lakini hawafanyi unachowaambia wafanye. Wanasema kwamba wana upendo, lakini hayo ni maneno matupu; wanachotafuta kwa moyo ni faida yao tu. Kwao, wewe umekuwa tu kama mwimbaji wa kutumbuiza mwenye sauti nzuri ikiandamana na muziki safi! Wanayasikia yale unayosema, lakini hawatekelezi hata mojawapo. Lakini hayo unayosema yatakapotukia — nayo kweli yatatukia — basi, ndipo watakapotambua kuwa nabii amekuwapo miongoni mwao.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Toa unabii dhidi ya wachungaji wa Israeli. Waambie hao wachungaji kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wenu nyinyi wachungaji wa Israeli, mnaojilisha nyinyi wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? Mnakunywa maziwa, mnavaa mavazi ya manyoya yao na kondoo wanono mnawachinja na kuwala. Lakini hamwalishi hao kondoo. Walio dhaifu hamkuwapatia nguvu, wagonjwa hamkuwaponya, waliojeruhiwa hamkuwafungia dawa, waliotangatanga hamkuwarudisha na waliopotea hamkuwatafuta. Lakini mmetumia mabavu na ukatili kuwatawala. Basi, kwa kuwa hao kondoo hawakuwa na mchungaji walitawanywa, wakawa mawindo ya wanyama wakali. Naam, kondoo wangu walitawanywa, wakatangatanga milimani na vilimani. Kondoo walisambazwa duniani kote, na hapakuwa na mtu aliyejali juu yao wala kuwatafuta. “Basi, sikieni vizuri neno langu mimi Mwenyezi-Mungu, enyi wachungaji: Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba: Nimechoka kuwaona kondoo wangu wamekuwa mawindo ya wanyama wakali kwa vile hapakuwa na mchungaji; wachungaji wangu hawakuwatafuta kondoo wangu, bali wamejilisha wao wenyewe badala ya kuwalisha kondoo wangu. Basi, nyinyi wachungaji, sikieni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitapambana nanyi, enyi wachungaji. Nitawaondolea madaraka ya kuchunga kondoo wangu, wala sitakubali muwachunge tena. Hamtakuwa tena na nafasi ya kujinufaisha wenyewe. Nitawaokoa kondoo wangu makuchani mwenu, ili wasiwe chakula chenu tena. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe nitawatafuta kondoo wangu na kuwatunza. Kama mchungaji anavyowatafuta kondoo wake waliotawanyika, ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu. Nitawarudisha kutoka kila mahali walipotawanyika siku yenye mawingu na giza nene. Nitawatoa kutoka kwa watu wa mataifa. Nitawakusanya kutoka nchi za mbali na kuwaleta katika nchi yao wenyewe. Nitawachunga juu ya milima ya Israeli, kando ya vijito na katika sehemu zote za nchi zinazokaliwa na watu. Nitawapa malisho mazuri kwenye milima mirefu ya Israeli ambako yako malisho yao. Watapumzika huko kwenye mbuga za malisho mazuri; naam, watapata malisho mazuri juu ya milima ya Israeli. Mimi mwenyewe nitakuwa mchungaji wa kondoo wangu. Mimi mwenyewe nitawapumzisha. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Kondoo waliopotea nitawatafuta na waliotangatanga nitawarudisha nyumbani. Waliojeruhiwa nitawatibu, na wale walio dhaifu nitawapa nguvu. Kondoo wanono na wenye nguvu nitawaangamiza. Mimi nitawachunga kondoo kama itakiwavyo. “Na Nyinyi mlio kundi langu, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitaamua baina ya kondoo na kondoo; baina ya kondoo dume na mbuzi. Baadhi yenu mnakula malisho mazuri na pia kukanyagakanyaga yale yaliyobaki! Mnakunywa maji safi na yanayobaki mnayachafua kwa miguu yenu! Je, kondoo wangu wengine wale malisho yaliyokanyagwakanyagwa na kunywa maji yaliyochafuliwa? “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambia hivi: Mimi mwenyewe nitaamua kati ya kondoo wanono na kondoo dhaifu. Nyinyi mnawasukuma kwa mbavu na kwa mabega na kuwapiga pembe kondoo wote walio dhaifu mpaka mmewatawanya mbali na kundi. Lakini mimi nitawaokoa kondoo wangu wasiwe tena mawindo. Nitatoa hukumu juu ya kila kondoo. Nitamweka mchungaji mmoja juu yao, mfalme kama mtumishi wangu Daudi. Yeye atawalisha na kuwa mchungaji wao. Nami Mwenyezi-Mungu, nitakuwa Mungu wao, naye mtumishi wangu Daudi atakuwa mkuu wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitafanya nao agano la amani. Nitaondoa wanyama wakali katika nchi, ili kondoo wangu wakae mbugani kwa usalama na kulala msituni. “Nitawafanya waishi kandokando ya mlima wangu mtakatifu na kuwabariki. Nitawaletea mvua kwa wakati wake, nazo zitakuwa mvua za baraka. Miti mashambani itazaa matunda, ardhi itatoa mazao kwa wingi, nao wataishi salama katika nchi yao. Nitakapovunja nira zao za utumwa na kuwaokoa mikononi mwa hao waliowafanya kuwa watumwa ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu Hawatakuwa tena mawindo ya mataifa mengine wala wanyama wa porini hawatawaua na kuwala. Wataishi kwa usalama na hakuna atakayewatisha. Nitawapa mashamba yenye rutuba ili wasiangamizwe tena na njaa nchini humo, wala kudharauliwa tena na mataifa mengine. Nao watajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, niko pamoja nao na kwamba watu hao wa Israeli ni watu wangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nyinyi, kundi la kondoo wangu, ni nyinyi watu wangu, nami ni Mungu wenu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Ugeukie mlima Seiri, utoe unabii juu ya wakazi wake. Uambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi napambana nawe, ee mlima Seiri. Ninanyosha mkono wangu dhidi yako na kukufanya uwe jangwa na ukiwa. Ninaifanya miji yako kuwa magofu nawe utakuwa jangwa. Ndipo utakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Ulikuwa adui wa daima wa Israeli, ukasababisha watu wake wauawe kwa upanga, wakati wa msiba wao, wakati wa adhabu yao ya mwisho. Kwa hiyo, kama niishivyo, nasema mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba kifo kinakungoja na hutaweza kukikwepa. Kwa kuwa unayo hatia ya mauaji, basi mauaji nayo yatakuandama. Nitaufanya mlima Seiri kuwa ukiwa na jangwa na yeyote apitaye huko nitamwangamiza. Nitajaza milima yako watu waliouawa; na katika vilima vyako na mabonde yako na magenge yako yote watakuwako waliouawa kwa upanga. Nitakufanya kuwa jangwa milele, na miji yako haitakaliwa tena. Ndipo utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Wewe ulisema ya kwamba mataifa hayo mawili yaani Yuda na Israeli ni mali yako na kwamba utazimiliki! Ulisema hivyo ingawa humo ni makao yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu naapa kwa nafsi yangu kwamba nitakutenda kadiri ya hasira na wivu wako, kulingana na chuki yako kwao. Nitakapokuadhibu utatambua mimi ni nani! Wewe utajua ya kwamba mimi mwenyewe Mwenyezi-Mungu nimeyasikia matusi yote uliyoyatoa dhidi ya milima ya Israeli, ukisema: ‘Milima ya Israeli imefanywa kuwa jangwa! Tumepewa sisi tuinyakue!’ Nimesikia jinsi unavyojigamba na kusema maneno mengi dhidi yangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitakapokufanya wewe Edomu kuwa jangwa, dunia yote itafurahi kama wewe ulivyofanya wakati nchi ya Waisraeli ilipoharibiwa. Utakuwa jangwa, ewe mlima Seiri, pamoja na nchi yote ya Edomu. Ndipo watu watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Wewe mtu! Toa unabii kuhusu milima ya Israeli. Iambie isikilize maneno yangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Maadui zenu wamewazomea na kusema kuwa nyinyi mmekuwa mali yao! “Kwa hiyo, wewe Ezekieli, toa unabii useme kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Watu wamewafanya nyinyi milima ya Israeli kuwa tupu na kuwavamia kutoka kila upande hata mmekuwa mali ya mataifa mengine, mkawa kitu cha kusimangwa na kudhihakiwa miongoni mwa watu! Kwa hiyo, enyi milima ya Israeli, sikieni neno langu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu: Nyinyi milima na vilima, mifereji na mabonde, nyika tupu na miji mmehamwa, mkatekwa nyara na kudharauliwa na mataifa yote yanayowazungukeni. Sasa kwa kuwa mimi nimechukizwa mno, nitayaadhibu mataifa mengine na hasa watu wa Edomu. Wao kwa furaha moyoni na madharau waliichukua hiyo nchi iliyo yangu iwe yao. Kwa hiyo, ewe mtu, toa unabii kuhusu nchi ya Israeli, uiambie milima na vilima, vijito na mabonde kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema mambo haya kutokana na ghadhabu yangu yenye wivu juu ya nchi yangu, kwa sababu imetukanwa na watu wa mataifa. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninaapa kwamba watu wa mataifa yaliyo jirani nanyi watatukanwa wao wenyewe. “Lakini kuhusu milima ya Israeli, miti itatoa matawi na kuzaa matunda kwa ajili ya watu wangu wa Israeli, maana wao watarudi makwao karibuni. Mimi niko upande wenu, nitahakikisha kuwa mnalimwa na kupandwa mbegu. Waisraeli nitawazidisha sana. Miji itakaliwa, na magofu yatajengwa upya. Nitawafanya watu na wanyama waongezeke na kuwa wengi. Nitawafanya nyinyi milima mkaliwe tena kama zamani. Nitawatendea mema mengi kuliko zamani. Nanyi mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nitawafanya watu wangu Israeli watembee juu yenu. Nanyi mtakuwa milki yao, wala hamtawafanya tena wafiwe na watoto wao. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa vile watu wamesema juu yenu kwamba mnakula watu, na mmelipokonya taifa lenu watoto wake, basi, sasa hamtakula tena watu wala kupokonya taifa lenu watoto wake. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Sitaruhusu tena mataifa yawatukane, wala kuwadharau tena. Hamtasababisha taifa lenu likose. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Waisraeli walipoishi katika nchi yao waliitia unajisi kwa mienendo na matendo yao. Niliyaona matendo yao kuwa sawa na mwanamke aliye najisi wakati wa siku zake. Niliwamwagia ghadhabu yangu kwa sababu ya damu waliyomwaga katika nchi na kwa sababu ya miungu ambayo kwayo nchi ilitiwa unajisi. Niliwatawanya kati ya mataifa, wakasambazwa katika nchi nyingine. Niliwaadhibu kadiri ya tabia yao na matendo yao. Hata walipokuwa miongoni mwa mataifa walilikufuru jina langu takatifu, hata watu wakasema hivi juu yao: ‘Tazama! Hawa ndio wale watu wa Mwenyezi-Mungu, lakini wamelazimika kuondoka katika nchi yake!’ Hiyo ilinifanya kuhangaika juu ya jina langu takatifu ambalo watu wa Israeli walilikufuru miongoni mwa mataifa walikokwenda. Basi, waambie Waisraeli kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninachotaka kufanya si kwa faida yenu nyinyi watu wa Israeli, bali ni kwa heshima ya jina langu takatifu mlilolikufuru miongoni mwa mataifa mlikokwenda. Nitalirudishia hadhi yake takatifu jina langu kuu mlilokufuru miongoni mwa mataifa. Hapo ndipo mataifa yatakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitawatumia nyinyi kuonesha utakatifu wangu mbele yao. Nitawaondoa nyinyi katika kila taifa na kuwakusanya kutoka nchi zote za kigeni; nitawarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtatakata uchafu wenu wote na sanamu za miungu yenu yote. Nitawapeni moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu. Nitauondoa kwenu moyo mgumu kama jiwe na kuwapa moyo wa utii. Nitatia roho yangu ndani yenu; nitawafanya mfuate kanuni zangu na kuzingatia maazimio yangu. Mtakaa katika nchi niliyowapa wazee wenu. Mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Nitawaokoa kutoka uchafu wenu wote. Nitaiamuru ngano iongezeke, wala sitawaletea njaa tena. Nitayazidisha matunda ya miti na mazao ya mashamba ili msiaibike tena kwa njaa kati ya mataifa. Kisha mtakapokumbuka mienendo yenu miovu na matendo yenu mabaya, mtajichukia wenyewe kwa sababu ya maovu yenu na machukizo mliyofanya. Lakini jueni kwamba sitafanya hivyo kwa ajili yenu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Oneni aibu na kufadhaika kwa sababu ya matendo yenu, enyi Waisraeli! “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile nitakapowasafisheni maovu yenu yote, nitaifanya miji yenu ikaliwe, nayo magofu yajengwe upya. Nchi iliyokuwa jangwa italimwa tena, hata atakayepita huko hataiona kuwa jangwa. Nao watu watasema: ‘Nchi hii iliyokuwa jangwa, sasa imekuwa kama bustani ya Edeni, nayo miji iliyokuwa ukiwa, mahame na magofu, sasa inakaliwa na watu, tena ina ngome!’ Hapo mataifa yaliyobaki kandokando yenu, yatatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu niliyejenga upya yaliyoharibiwa na kupanda mbegu katika nchi iliyokuwa jangwa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema, na nitafanya hayo. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Waisraeli wataniomba niwafanye kuwa wengi kama kundi la kondoo, nami nitawafanya hivyo. Wataniomba wawe wengi kama kundi la kondoo wa tambiko, naam, kama kundi la kondoo mjini Yerusalemu wakati wa sikukuu zake. Hivyo ndivyo miji yenu iliyokuwa ukiwa itakavyojaa makundi ya watu. Hapo ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Mimi Ezekieli nilikumbwa na uzito wa nguvu ya Mwenyezi-Mungu, naye akaninyanyua kwa roho yake na kuniweka katika bonde lililokuwa limejaa mifupa. Basi, akanitembeza kila mahali bondeni humo. Kulikuwa na mifupa mingi sana katika bonde lile, nayo ilikuwa mikavu kabisa. Mwenyezi-Mungu akaniuliza, “Wewe mtu! Je, mifupa hii yaweza kuishi tena?” Nami nikamjibu, “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, wewe wajua!” Naye akaniambia, “Toa unabii juu ya mifupa hii. Iambie hivi: Enyi mifupa mikavu, sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu. Bwana Mwenyezi-Mungu awaambia hivi: Nitaifanya pumzi iwaingie, nanyi mtaishi. Nitawatia mishipa na nyama, nitawafunika ngozi na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi. Hapo mtajua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Basi, nikatoa unabii kama nilivyoamriwa. Nilipokuwa nikitoa unabii, kukatokea kelele kama ya mkwaruzo na ile mifupa ikaanza kusogeleana na kuungana. Nilitazama, nikaona ile mifupa imewekewa mishipa na nyama na kufunikwa kwa ngozi. Lakini haikuwa na uhai. Hapo, Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Ewe mtu, kwa niaba yangu toa unabii kwa upepo, ukauambie kwamba Bwana Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Ewe upepo njoo toka pande zote nne na kuipuliza miili hii iliyokufa ili ipate kuishi.” Basi, mimi nikatoa unabii kama alivyoniamuru, nayo pumzi ikaingia ndani yao, nayo ikawa hai, ikasimama: Kundi kubwa ajabu. Hapo Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Wewe mtu! Mifupa hiyo ni watu wote wa Israeli. Wao, wanasema, ‘Mifupa yetu imenyauka, matumaini yetu yamepotea nasi tumekwisha kabisa.’ Kwa hiyo, toa unabii, uwaambie, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Enyi watu wangu, nitayafunua makaburi yenu na kuwafufua kutoka makaburini mwenu. Nitawarudisha nyumbani kwenu katika nchi ya Israeli. Nanyi, enyi watu wangu, mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu nitakapofunua makaburi yenu na kuwafufua kutoka makaburini mwenu. Nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawaweka katika nchi yenu wenyewe. Hapo mtatambua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nimesema, nami nitafanya hayo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia; “Wewe mtu! Chukua kijiti kimoja, uandike juu yake maneno haya: ‘Kwa Yuda na Waisraeli wanaohusiana naye.’ Kisha chukua kijiti kingine, uandike juu yake maneno haya: ‘Kwa Yosefu (kijiti cha Efraimu) na Waisraeli wanaohusiana naye.’ Halafu vichukue vijiti hivyo na kuvishikamanisha ili vionekane kama kijiti kimoja. Wananchi wenzako watakapouliza, ‘Je, hutatueleza maana ya jambo hilo?’ Wewe utawajibu, Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nitakitwaa kijiti cha Yosefu (kilichomo mkononi mwa Efraimu) na makabila ya Israeli yanayounganika naye, nami nitakishikamanisha na kijiti cha Yuda ili vijiti hivyo viwili vifanywe kijiti kimoja mkononi mwangu. “Ukiwa mbele yao huku umeshika vijiti ulivyoandika juu yake, waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawatoa Waisraeli kutoka mataifa walikokwenda; nitawakusanya toka pande zote na kuwarudisha katika nchi yao. Nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi juu ya milima ya Israeli; mfalme mmoja atakuwa mfalme wao wote. Hawatakuwa tena mataifa mawili wala hawatagawanyika tena kuwa falme mbili. Hawatajitia unajisi tena kwa sanamu za miungu yao na kwa mambo yao ya kuchukiza wala kwa makosa yao. Nitawaokoa wasiwe tena waasi. Nao watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao. Mtumishi wangu Daudi atakuwa mfalme wao; naam, watakuwa na mchungaji mmoja tu. Watayafuata maagizo yangu na kuzingatia kanuni zangu. Watakaa katika nchi ya wazee wao ambayo nilimpa Yakobo. Wao na watoto wao na wajukuu wao wataishi humo milele. Naye Daudi, mtumishi wangu, atakuwa mtawala milele. Nitafanya nao agano la amani, nalo litakuwa agano la milele. Nitawabariki na kuwafanya wawe wengi, na maskani yangu nitaiweka kati yao milele. Nitaishi kati yao; nitakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wangu. Nayo mataifa yatatambua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, nimewatakasa Waisraeli na kwamba maskani yangu ipo kati yao milele.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Mgeukie Gogu mfalme wa nchi ya Magogu ambaye ni mtawala mkuu wa Mesheki na Tubali. Toa unabii juu yake na kumwambia kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi nitapambana nawe ewe Gogu mtawala wa Mesheki na Tubali. Mimi nitakuzungusha na kukutia ndoana matayani mwako, na kukutoa nje wewe pamoja na jeshi lako lote: Farasi na wapandafarasi na kundi kubwa la watu wamevaa mavazi ya vita, ngao na vigao mikononi, wanapunga mapanga yao. Wanajeshi kutoka Persia, Kushi na Puti wako pamoja nao; wote wana ngao na kofia za chuma. Pia vikosi kutoka Gomeri, Beth-togarma, upande wa kaskazini kabisa, na majeshi yao yote pamoja na majeshi kutoka mataifa mengine, yako pamoja nawe. Jitayarishe, ukae wewe mwenyewe na jeshi lako lote pamoja na wengine wote ulio nao, ukawalinde. “Baada ya siku nyingi utaitwa kuishambulia nchi ambayo watu wengi waliletwa kutoka mataifa mengi na sasa wanaishi bila vitisho vya vita. Utaishambulia milima ya Israeli ambayo hapo awali ilikuwa jangwa na mahame kwa muda mrefu, lakini sasa watu wote huko wanaishi kwa usalama. Utakwenda kasi kama tufani na kuifunika nchi kama wingu, wewe mwenyewe na jeshi lako lote na mataifa mengi yaliyo pamoja nawe. “Wewe Gogu! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile itakapofika utaanza kuwaza moyoni mwako na kupanga mipango miovu na kusema: ‘Nitakwenda kuishambulia nchi isiyo na kuta, nchi ambako wananchi wake wanaishi kwa amani. Wote wanakaa katika miji isiyo na kuta; hawana makomeo wala malango.’ Utapora na kuteka mali za watu wanaokaa katika miji ambayo ilikuwa jangwa. Watu hao wamekusanywa kutoka mataifa na sasa wana mifugo na mali; nao wanakaa kwenye kitovu cha dunia. Wakazi wa Sheba na Dedani pamoja na wafanyabiashara wa Tarshishi na vitongoji vyake watakuuliza, ‘Je, umekuja kuteka nyara? Je, umekusanya jeshi lako ili kushambulia na kutwaa nyara na kuchukua fedha na dhahabu, mifugo na bidhaa, na kuondoka na nyara nyingi?’ “Kwa hiyo, ewe mtu, toa unabii na kumwambia Gogu kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wakati taifa langu la Israeli linaishi kwa usalama, wewe utafunga safari kutoka kwenye maskani yako, huko mbali kabisa kaskazini, uje pamoja na watu wengi wakiwa wote wamepanda farasi: Jeshi kubwa na lenye nguvu. Utawakabili Waisraeli, kama wingu linalotanda juu ya nchi. Wakati huo nitakutuma uishambulie nchi yangu, ili mataifa yajue kwamba nimekutumia wewe Gogu ili nioneshe utakatifu wangu mbele yao. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema kwamba, wewe ndiwe niliyesema habari zako hapo kale kwa njia ya watumishi wangu manabii wa Israeli, ambao walitabiri nyakati zile kuwa baadaye nitakuleta upambane na watu wa Israeli.” Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Siku ile Gogu atakapoishambulia nchi ya Israeli, nitawasha ghadhabu yangu. Mimi natamka rasmi kwa wivu na ghadhabu yangu kali kwamba siku hiyo kutakuwa na tetemeko kubwa la ardhi nchini Israeli. Samaki baharini na ndege warukao, wanyama wa porini, viumbe vyote vitambaavyo pamoja na watu wote duniani, watatetemeka kwa kuniona. Milima itaporomoshwa, magenge yataanguka na kuta zote zitaanguka chini. Nami nitasababisha kila namna ya tisho kumkabili Gogu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Wanajeshi wake wataanza kushambuliana wenyewe kwa mapanga yao. Nitamwadhibu Gogu kwa magonjwa mabaya na mauaji. Nitanyesha mvua nyingi, mvua ya mawe na moto wa madini ya kiberiti juu yake, juu ya vikosi vyake, na mataifa yale mengi yaliyo pamoja naye. Ndivyo nitakavyofanya mataifa yote yaone ukuu wangu na utakatifu wangu. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Bwana Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Wewe mtu! Toa unabii dhidi ya Gogu. Mwambie, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi nitapambana nawe Gogu mtawala mkuu wa mataifa ya Mesheki na Tubali. Nitakugeuza na kukuelekeza upande mwingine na kukuongoza kutoka mbali kaskazini uende kushambulia milima ya Israeli. Kisha nitauvunja upinde wako katika mkono wako wa kushoto, na mishale yako katika mkono wako wa kulia nitaiangusha chini. Utakufa juu ya milima ya Israeli, wewe pamoja na vikosi vyako vyote na mataifa yaliyo pamoja nawe. Nami nitaitoa miili yao iliwe na ndege wa kila aina na wanyama wakali. Utafia porini. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitapeleka moto juu ya Magogu na juu ya wote wakaao salama katika nchi za pwani. Nao watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nitalifanya jina langu takatifu litambuliwe na watu wangu Israeli, wala sitaruhusu tena watu walikufuru jina langu takatifu. Nayo mataifa yatatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli. “Siku ile ninayosema juu yake kwa hakika inakuja. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Hapo, watu waishio katika miji ya Israeli watatoka na kukusanya silaha zilizoachwa na kuzichoma moto. Watatumia hizo ngao, pinde, mishale, mikuki na marungu, kama kuni za kuwasha moto kwa muda wa miaka saba. Hawatahitaji kuokota kuni mashambani, wala kukata miti msituni, kwani watazitumia hizo silaha kuwashia nazo moto. Watapora mali za wale waliopora mali zao na kuwapokonya wale waliopokonya mali zao. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Katika siku ile, nitampa Gogu mahali pa kuzikwa katika nchi ya Israeli, katika Bonde la Wasafiri, upande wa mashariki wa bahari ya Chumvi. Gogu atazikwa huko pamoja na jeshi lake lote, nao wasafiri watazuiwa kupita huko. Bonde hilo litaitwa, ‘Bonde la Hamon-gogu’. Kwa kuisafisha nchi Waisraeli watatumia muda wa miezi saba kuzika maiti hizo. Watu wote nchini watashughulika kuwazika. Na hilo litakuwa jambo la kuwapatia sifa, siku ile nitakapodhihirisha utukufu wangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Baada ya miezi hiyo saba, watachagua watu wapitepite nchini kutafuta maiti ambazo zitakuwa bado hazijazikwa, wazizike ili kuisafisha nchi. Wakati wanapopitapita humo nchini, kama wakiona mfupa wa binadamu wataweka alama ili wale wanaozika waje na kuuzika katika Bonde la Hamon-gogu. Huko kutakuwa pia mji utakaoitwa Hamona. Ndivyo watakavyoisafisha nchi. “Sasa, ewe mtu, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Waite ndege wote na wanyama wote wa porini wakusanyike toka pande zote na kuja kula karamu ya kafara ninayowaandalia, ambayo itakuwa kubwa sana juu ya milima ya Israeli, ambako watakula nyama na kunywa damu. Watakula nyama ya mashujaa, watakunywa damu ya wakuu wa dunia watakaochinjwa kama kondoo madume au wanakondoo, mbuzi au mafahali wanono wa Bashani. Katika karamu hiyo ninayowafanyia watakula mafuta na kushiba. Watakunywa damu na kulewa. Mezani pangu, watashibishwa kwa farasi, wapandafarasi, mashujaa na watu wote wa vita. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Nitayafanya mataifa yote yauone utukufu wangu, na kuwaonesha jinsi ninavyotumia nguvu yangu kutekeleza hukumu zangu za haki. Waisraeli watajua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, tangu siku hiyo na baadaye. Mataifa yatajua kuwa Waisraeli walikwenda uhamishoni kutokana na makosa yao wenyewe waliyonikosea. Waliniasi, nami nikageuka wasinione, nikawaweka mikononi mwa maadui zao wakauawa. Niligeuka wasinione, nikawatenda kulingana na uchafu na makosa yao. “Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Sasa nitawahurumia Waisraeli wazawa wa Yakobo, na kuwarudishia fanaka yao. Daima nataka jina langu takatifu liheshimiwe. Watakapokuwa wanaishi kwa usalama katika nchi yao, bila ya kutishwa, watasahau aibu yao na uasi walionitenda. Wakati huo, nitakuwa nimewarudisha kutoka kwa mataifa na kuwakusanya kutoka nchi za maadui zao na kudhihirisha utakatifu wangu mbele ya mataifa mengi. Kisha watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, kwa sababu mimi niliwapeleka uhamishoni kati ya mataifa na kuwarudisha tena katika nchi yao. Sitamwacha hata mtu wao abaki miongoni mwa mataifa. Nitakapowamiminia Waisraeli roho yangu, sitageuka tena wasinione. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwaka wa ishirini na tano tangu kuhamishwa kwetu, siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, siku hiyo niliusikia uzito wa nguvu ya Mwenyezi-Mungu. Ilikuwa mwaka wa kumi na nne tangu mji wa Yerusalemu ulipotekwa. Basi, nikiwa katika njozi Mwenyezi-Mungu alinichukua mpaka nchini Israeli, akaniweka juu ya mlima mrefu sana, na upande wa kusini kulikuwa na majengo yaliyoonekana kama mji. Basi, alinipeleka huko, nami nikamwona mtu aliyeonekana anangara kama shaba. Mikononi mwake mtu huyo alikuwa na kamba ya kitani ya kupimia pamoja na ufito wa kupimia, naye alikuwa amesimama karibu na lango. Basi, akaniambia: “Wewe mtu! Tazama vizuri na kusikiliza kwa makini. Zingatia kwa moyo uone kila kitu nitakachokuonesha maana umeletwa hapa ili nikuoneshe kitu. Unapaswa kuwatangazia watu wa Israeli kila kitu utakachoona.” Basi, huko, niliona hekalu nalo lilikuwa limezungukwa na ukuta upande wa nje. Yule mtu akauchukua ufito wake wa kupimia ambao ulikuwa na urefu wa mita 3, akaupima ule ukuta. Ukuta huo ulikuwa na kimo cha mita 3 na unene wa mita 3. Kisha, akaenda kwenye lango la mashariki akapanda ngazi na akiwa juu akapima kizingiti cha lango ambacho kilikuwa na kina mita 3. Kulikuwa na vyumba vya walinzi kila upande wa nafasi ya kupitia na kila kimoja kilikuwa cha mraba: Urefu mita 3 upana mita 3. Kuta zilizotenganisha vyumba hivyo zilikuwa na unene mita 2.5. Kulikuwa na ukumbi mrefu wa mita 3 ambao ulielekea kwenye chumba kikubwa mkabala na hekalu. Yule mtu akakipima pia chumba hicho, nacho kilikuwa na kina mita 4. Halafu akapima kuta zake za nje zikaonekana zina unene wa mita moja. Sehemu ya ndani ya lango ilikuwa sehemu iliyokuwa karibu zaidi na hekalu. Kulikuwa na sehemu ya kuingilia iliyokuwa na vyumba vitatu vya walinzi, kila upande na vyote vilikuwa na ukubwa uleule; nazo kuta zilizovitenganisha zilikuwa na unene uleule. Kisha, yule mtu akapima upana wa nafasi ya kupitia katika lango. Upana wake ulikuwa mita 6.5. Ukubwa wote wa ukumbi wa katikati wa kupitia ulikuwa mita 5. Mbele ya vyumba vya walinzi ambavyo vilikuwa mraba: Mita 3 kwa 3, kulikuwa na ukuta mfupi kama kizuizi ukiwa na kimo cha sentimita 50 na unene sentimita 50. Yule mtu akapima umbali kutoka ukuta wa nyuma wa chumba kimojawapo hadi kwenye ukuta wa nyuma ya chumba upande wa pili penye nafasi ya kupitia, akapata mitakumi na mbili u nusu. Chumba cha mwisho kabisa kilielekea kwenye ua. Akakipima chumba hicho nacho kilikuwa na upana mita 10. Kutoka mbele ya lango kwenye mwingilio mpaka ukumbi wa ndani wa lango kulikuwa na mita 25. Kulikuwa na matundu madogomadogo kwenye miimo ya nje ya vyumba vyote na hata kwenye kuta zilizotenganisha vyumba. Kulikuwa na michoro ya mitende kwenye miimo ya ndani iliyoelekea ukumbi wa kupitia. Kisha yule mtu akanipeleka mpaka ua wa nje ya hekalu. Huko kulikuwa na vyumba thelathini kuuzunguka ukuta wa nje na mbele ya vyumba hivyo kulikuwa na sakafu ya mawe. Sakafu hiyo ilitandazwa kuzunguka malango kwa kufuatana na urefu wa malango hayo; hiyo ilikuwa sakafu ya chini. Baadaye, yule mtu akapima umbali wa njia iliyokuwa ikitoka kwenye ua wa ndani wa sehemu ya chini ikielekea nje ya ua huo, akapata mita 50. Kisha, yule mtu akapima urefu na upana wa lango la upande wa kaskazini wa ua wa nje. Kulikuwa na vyumba vitatu vya walinzi kila upande wa lango, vipimo vya miimo yake na matao yake vilikuwa kama vile vya lango la kwanza. Urefu wote wa ile njia ulikuwa kwa jumla mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Chumba cha kuingilia na madirisha na matao yake, pia ile mitende iliyochorwa ukutani, vyote vilifanana na vile vya lango la mashariki. Hapo palikuwa na ngazi saba za kupandia kwenye lango, na matao yake yalikuwa mbele yake. Kutoka hapo penye njia ya kuingilia ya kaskazini na kuvuka huo ua moja kwa moja kulikuwa na njia nyingine ya kuingilia iliyoelekea kwenye ua wa ndani, kama ilivyokuwa upande wa mashariki. Yule mtu alipima urefu wa kutoka njia mpaka njia, akapata mita 50. Yule mtu akanichukua upande wa kusini; huko nako kulikuwako lango; alipima miimo yake na ukumbi na vipimo vyake vilikuwa sawa na miimo na kumbi nyingine. Kulikuwa na madirisha pande zote kama ilivyokuwa katika vyumba vingine. Urefu wake ulikuwa mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia kwenye njia hiyo ya kuingilia na mwishoni mwake kulikuwa na ukumbi uliokuwa mkabala na ua. Kulikuwa na michoro ya mitende kwenye kuta za ndani zilizokuwa mkabala na hiyo njia ya kuingilia. Mkabala na njia hiyo ya kuingilia kulikuwa na njia ya kuingilia kwenye ua wa ndani. Yule mtu akapima urefu kati ya hizo njia, akapata mita 50. Yule mtu akanipitisha kwenye njia ya kuingilia upande wa kusini, tukafika kwenye ua wa ndani. Aliipima hiyo njia nayo ilikuwa sawa na zile njia nyingine za kuingilia kwenye kuta za nje. Vyumba vya walinzi, ukumbi, na kuta zake vilikuwa na ukubwa uleule kama vile vingine; kulikuwa na madirisha pia kandokando ya hiyo njia ya kuingilia na kwenye ukumbi. Ilikuwa na urefu mita 25 na upana mita kumi na mbili u nusu. Kulikuwa na vyumba kandokando ya hiyo njia ya kuingilia, vikiwa na urefu wa mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Ule ukumbi ulikuwa mkabala na ua wa nje. Na kulikuwa na michoro ya mitende kwenye nguzo kandokando ya hiyo njia ya kuingilia kwenye ngazi. Kulikuwa na ngazi nane za kupandia lango hili. Yule mtu alinipeleka upande wa mashariki wa ua wa ndani. Akaipima ile njia ya kuingilia, nayo ilikuwa na urefu kama zile njia nyingine za kuingilia. Vyumba vyake vya walinzi, nguzo zake za ndani pamoja na ukumbi vilikuwa na ukubwa kama vile vingine. Kulikuwa na madirisha pande zote hata kwenye matao na chumba cha kuingilia. Urefu wake ulikuwa mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Kile chumba cha kuingilia kilikuwa mkabala na uwanja wa nje. Mitende ilichorwa kwenye kuta kwenye nafasi ya kupitia. Kulikuwa na ngazi nane za kupandia kuelekea kwenye lango hili. Kisha yule mtu akanipeleka kwenye njia ya kuingilia upande wa kaskazini. Basi, akaipima hiyo njia ya kuingilia, nayo ilikuwa sawa na zile njia nyingine. Huko nako kulikuwa na vyumba vya walinzi, kuta za ndani zilizopambwa, ukumbi wa kuingilia na madirisha pande zote. Urefu wake wote ulikuwa mita 25 na upana mita kumi na mbili u nusu. Ule ukumbi wa kuingilia ulikuwa mkabala na ua wa nje; kulikuwa na mitende imechorwa kwenye kuta za hiyo nafasi ya kupitia. Pia kulikuwa na ngazi nane za kupandia kuelekea kwenye lango hili. Kwenye ua wa nje, kulikuwa na chumba cha ziada kilichounganishwa na njia ya kuingilia ya ndani, upande wa kaskazini. Chumba hicho kilikuwa mkabala na ukumbi wa kuingia, na huko walisafishia wanyama waliochinjwa kwa ajili ya tambiko za kuteketezwa nzima. Halafu katika ukumbi karibu na njia kulikuwako meza mbili upande mmoja na nyingine mbili upande mwingine. Meza hizo zilitumika kuwa mahali pa kuchinjia sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuondoa hatia. Nje ya ukumbi huo, kulikuwa na meza mbili upande mmoja na mbili upande mwingine wa njia ya kuingilia kwenye lango la kaskazini. Meza zote ambazo zilitumiwa kwa kuchinjia wanyama wa tambiko zilikuwa nane: Meza nne ndani ya ukumbi na meza nne nje ya ukumbi. Kulikuwako pia meza nne ndani ya ukumbi zilizotumiwa kuandalia sadaka za kuteketezwa. Meza hizo zilikuwa zimejengwa kwa mawe yaliyochongwa. Kimo cha kila meza kilikuwa sentimita 50 na upande wake wa juu ulikuwa mraba wenye upana wa sentimita 75. Vifaa vyote vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na sadaka nyingine viliwekwa juu ya meza hizo. Ndani ya ukumbi huo palizungukwa na vijiti vya kutundikia urefu wa kitanga, na nyama ziliwekwa mezani. Nje ya njia ya ndani kulikuwako vyumba vya walinzi kwenye ua wa ndani uliokuwa upande wa kaskazini wa njia. Vyumba hivyo vilielekea upande wa kusini. Chumba kimoja kilichokuwa upande wa lango la mashariki kilielekea upande wa kaskazini. Yule mtu akaniambia, “Chumba hiki kinachoelekea kusini ni kwa ajili ya makuhani wanaohudumu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na chumba kinachoelekea kaskazini ni kwa ajili ya makuhani wanaohudumu madhabahuni. Makuhani hawa ni wale wa ukoo wa Sadoki, ndio hao kati ya watu wa kabila la Lawi wanaoruhusiwa kwenda mbele ya Mwenyezi-Mungu.” Yule mtu akaupima ua wa ndani, nao ulikuwa mraba: Pande zote zilikuwa na upana wa mita 50. Madhabahu yalikuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Baadaye, alinipeleka kwenye ukumbi wa kuingilia nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Akalipima lango, nalo lilikuwa na kimo cha mita 2.5 na upana wa mita 7. Na kuta zake zilikuwa na unene mita 1.5 kila upande. Kulikuwa na ngazi za kupandia kwenye ukumbi wa chumba cha kuingilia, ambao ulikuwa na upana wa mita 10 na kina cha mita 6. Kulikuwa na nguzo mbili, nguzo moja kila upande wa mlango. Kisha, yule mtu akanipeleka kwenye ukumbi wa ndani, mahali patakatifu. Akaipima nafasi iliyoelekea humo ndani, nayo ilikuwa na kina cha mita 3, na upana wa mita 5. Nafasi hiyo ilikuwa na kuta kila upande zenye unene wa mita 2.5. Akaupima ukumbi wenyewe, nao ulikuwa na urefu wa mita 20 na upana mita 10. Kisha akaenda kwenye chumba cha ndani kabisa. Akaipima nafasi iliyoelekea huko, nayo ilikuwa na kimo cha mita 1 na upana mita 3.5. Nafasi hiyo ilikuwa na kuta kila upande zenye unene wa mita tatu u nusu. Akakipima chumba chenyewe, nacho kilikuwa cha mraba pande zake zikiwa na upana wa mita 10. Chumba hiki kilikuwa mbele ya ukumbi wa katikati. Kisha, akaniambia, “Hapa ndipo mahali patakatifu kabisa.” Yule mtu aliupima unene wa ukuta wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nao ulikuwa mita tatu. Kulikuwa na mfululizo wa vyumba vidogovidogo kuizunguka nyumba ya Mwenyezi-Mungu, vyenye upana wa mita mbili. Vyumba hivi, vilikuwa katika majengo ya ghorofa tatu, na kila ghorofa ilikuwa na vyumba thelathini. Ukuta wa nje wa hekalu kila kwenye ghorofa ulikuwa mwembamba kuliko ule wa ghorofa ya chini, ili vile vyumba viwe imara bila ya kuutegemea ukuta wa hekalu. Kwa upande, zile kuta za hekalu zikitazamwa kutokea nje, zilionekana kuwa na unene uleule toka chini hadi juu. Mkabala na ukuta wa nje wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nje ya vyumba, kulikuwa na ngazi mbili, ambazo zilifanya iwe rahisi kwenda juu kutokea ghorofa ya chini hadi ile ya juu. Kisha, nikaona kuwa hekalu lilikuwa na sakafu iliyonyanyuliwa kulizunguka, nayo ilikuwa ndio msingi wa zile ghorofa tatu mkabala na hekalu, kimo cha msingi wa ghorofa hizo ulikuwa sawa na ule ufito wa kupimia, mita tatu. Unene wa ukuta wa nje wa vyumba vya ndani ulikuwa mita mbili u nusu. Nafasi wazi kati ya vyumba vya pembeni mkabala na hekalu na vyumba vya walinzi vilikuwa na upana wa mita 10, kuzunguka hekalu. Kulikuwa na milango kwenye vyumba vya pembeni kutokea kwenye uwanja, mmoja upande wa kaskazini na mwingine upande wa kusini. Na msingi uliounganishwa na uwanja ulikuwa na upana wa mita 2.5. Mwishoni kabisa mwa uwanja, upande wa magharibi kulikuwa na jengo lenye urefu wa mita 45 na upana wa mita 35. Kuta zake zilikuwa na unene wa mita 2.5. Yule mtu akapima upande wa nje wa hekalu nao ulikuwa na urefu wa mita 50. Tokea nyuma ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kupitia ile nafasi ya kupitia, hadi mwisho wake, upande wa magharibi, umbali wake ulikuwa pia mita 50. Urefu mbele ya hekalu tangu upande huu hadi upande huu ukichanganya na ile nafasi wazi, ulikuwa pia mita 50. Yule mtu akapima urefu wa jengo hadi magharibi pamoja na mabaraza yake pande zake zote, nalo lilikuwa na urefu wa mita 50. Chumba cha kuingilia hekaluni, mahali patakatifu, na mahali patakatifu kabisa, vyote vilipambwa kwa mbao tangu sakafuni hadi kwenye madirisha. Madirisha haya yangeweza kufunikwa. Mpaka kwenye nafasi juu ya mlango hata kwenye chumba cha ndani na nje yake, pia juu ya kuta ndani ya chumba cha ndani na kwenye ukumbi palikuwapo na michoro iliyofanana na mitende na picha za viumbe wenye mabawa. Kila baada ya mtende kulichorwa picha ya kiumbe chenye mabawa kukizunguka chumba chote. Kila kiumbe alikuwa na nyuso mbili: Uso wa mwanadamu ulioelekea kwenye mtende upande mmoja na uso wa simba ulioelekea kwenye mtende wa upande mwingine. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwenye nyumba nzima, tangu sakafu hadi juu ya milango palichorwa viumbe wenye mabawa na mitende. Miimo ya mahali patakatifu ilikuwa ya mraba. Mbele ya mlango wa kuingilia mahali patakatifu kabisa kulikuwa na kitu kilichoonekana kama madhabahu ya mbao. Kimo chake kilikuwa nusu mita na upana wa mita moja. Pembe zake, tako lake, na pande zake zote zilikuwa zimetengenezwa kwa mbao. Yule mtu akaniambia, “Hii ndiyo meza inayokaa mbele ya Mwenyezi-Mungu.” Kulikuwako na mlango wa tarabe wa kuingia kwenye ukumbi wa hekalu na mlango wa tarabe wa kuingia mahali patakatifu kabisa. Milango hiyo ilikuwa ya tarabe, kwa hiyo kila mlango uliweza kufunguka katikati. Kwenye mlango wa kuingilia ukumbi kulichorwa viumbe vyenye mabawa na mitende, kama ilivyokuwa kwenye kuta. Na kulikuwa na kifuniko cha ubao kikifunika mlango kwa nje kwenye sehemu ya kuingilia ndani. Pembeni mwa chumba hiki, kulikuwa na madirisha madogo na kuta zilipambwa kwa michoro ya mitende. Kisha yule mtu alinipeleka kwenye uwanja wa nje hadi kwenye jengo lililokuwa upande wa kaskazini, naye akaniingiza kwenye vyumba vilivyokabili ua wa hekalu na jengo lililokuwa upande wa kaskazini. Jengo hili lililokuwa upande wa kaskazini lilikuwa na urefu wa mita 50 na upana wa mita 25. Kulikuwako ghorofa tatu zilizounganisha mita 10 za ua wa ndani na zikiwa mkabala wa sakafu ya ua wa nje. Upande wa kaskazini wa jengo hilo, kulikuwa na njia ya kupitia yenye upana wa mita 5 na urefu wake mita 50. Milango yake ilikuwa upande wa kaskazini. Vyumba vya juu vilikuwa vyembamba kuliko vile vya katikati na vya chini kwani vilikuwa mbali zaidi. Vile vyumba vya juu kabisa vilijengwa kwenye miinuko na havikusaidiwa na nguzo kama majengo mengine kwenye ua wa nje. Kulikuwa na ukuta mkabala na vyumba kuelekea uwanja wa nje ukiwa na urefu wa mita 25. Wakati vyumba kwenye ua wa nje vikiwa na urefu wa mita 20, vile vya mkabala na hekalu vilikuwa na urefu wa mita 50. Chini ya vyumba hivi kulikuwa na njia ya kupitia tokea upande wa mashariki mwishoni mwa jengo, ikiwa mtu anaingia tokea ua wa nje ambako ukuta wa nje unaanzia. Kwenye upande wa kusini kulikuwa na jengo lingine sawa na lile lingine si mbali na jengo la upande wa magharibi mwishoni mwa hekalu. Mbele ya vyumba hivyo kulikuwa na njia ya kupitia kama ile ya upande wa kaskazini. Jengo hilo lilikuwa na vipimo vilevile kama vya lile lingine, ramani na miinuko yake ilifanana na ile nyingine. Kulikuwa na mlango chini ya vyumba kwenye upande wa kusini wa jengo, mwishoni mwa upande wa mashariki ambako ukuta ulianzia. Yule mtu akaniambia, “Vyumba hivi vyote ni vitakatifu. Ndani ya vyumba hivi makuhani wanaoingia mbele ya Mwenyezi-Mungu, wanakula sadaka takatifu kabisa: Tambiko takatifu kabisa na humo ndimo mnamowekwa sadaka za nafaka, sadaka za kuondoa dhambi na sadaka za kuondoa hatia kwa kuwa mahali hapo ni patakatifu. Makuhani ambao watakuwa wamehudumu katika patakatifu, wanapotaka kwenda kwenye ua wa nje, ni lazima wayaache humo mavazi waliyovaa walipokuwa wanahudumu mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa sababu mavazi hayo ni matakatifu. Ni lazima wavae mavazi mengine kabla ya kutoka nje ambako watu wanakusanyika.” Baada ya yule mtu kulipima eneo la ndani la nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alinitoa nje kupitia lango la mashariki na kulipima eneo la nje. Aliuchukua ule ufito wake wa kupimia na kuupima upande wa mashariki, nao ulikuwa mita 250. Akaupima upande wa kaskazini kwa kutumia ufito wake, nao ulikuwa mita 250. Kisha akaupima upande wa kusini kwa kutumia ufito wake, nao ulikuwa mita 250. Kisha akageuka na kupima upande wa magharibi kwa kutumia ufito wake, nao ulikuwa mita 250. Hivyo akawa amepima pande zote, nazo zilikuwa mita 250 kila upande. Ukuta huo ulitenganisha kati ya eneo takatifu na lile la kawaida. Kisha, yule mtu akanipeleka kwenye lango linaloelekea mashariki. Utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea upande wa mashariki. Pamoja nao kulikuwapo mshindo wa kuja kwake kama mshindo wa maji mengi, nchi ilingaa kwa utukufu wake. Maono hayo yalikuwa kama maono niliyoyaona Mungu alipokuja kuuangamiza mji wa Yerusalemu. Pia yalifanana na maono niliyoyaona karibu na mto Kebari. Nikaanguka kifudifudi. Nao utukufu wa Mwenyezi-Mungu uliingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa njia ya lango la mashariki. Kisha roho ya Mungu ikaninyanyua na kunipeleka kwenye uwanja wa ndani. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukiwa umeijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Yule mtu akiwa anasimama karibu nami, nilisikia mtu fulani akisema kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu; naye akaniambia, “Wewe mtu! Hapa ndipo mahali pa kiti changu cha enzi, mahali niwekapo nyayo za miguu yangu. Nitakaa miongoni mwa watu wa Israeli milele. Na Waisraeli hawatalitia unajisi jina langu, wao wenyewe, wala wafalme wao kwa kuziabudu sanamu au kuzika maiti za wafalme wao mahali hapa. Wafalme wao walijenga vizingiti na miimo ya ikulu zao karibu na vizingiti vya nguzo za hekalu langu, hivyo kati yangu na wao ulikuwa ni ukuta tu. Walilitia unajisi jina langu takatifu kwa machukizo yao waliyotenda, ndiyo maana nimewaangamiza kwa hasira yangu. Sasa na waache kuziabudu sanamu na waziondoe maiti za wafalme wao mbali nami, nami nitakaa miongoni mwao milele. “Sasa, ewe mtu, waeleze Waisraeli habari za nyumba ya Mungu na wajifunze ramani yake. Waaibike kutokana na machukizo yao waliyotenda. Wakiona aibu kutokana na matendo yao, waeleze ramani ya nyumba ya Mungu: Ramani yake yenyewe, milango ya kuingilia na kutokea, umbo lake lote, mipango ya kila kitu, kanuni zake na masharti yake. Waandikie hayo yote waziwazi ili waweze kuona yote yalivyopangwa na waweze kuzifuata kanuni na masharti yake. Hii ndiyo sheria kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Eneo lote linalozunguka nyumba ya Mwenyezi-Mungu juu ya mlima lazima liwe takatifu kabisa.” Vipimo vya madhabahu, vitakuwa vilevile kama vipimo vya hekalu. Kuuzunguka msingi wa madhabahu, kutakuwa na mfereji wenye kina cha sentimita 50 na upana wa sentimita 50, pamoja na ukingo wenye kina cha sentimita 25. Sehemu ya madhabahu itakayokuwa chini kabisa tokea juu ya msingi itakuwa na kimo cha mita 1. Sehemu itakayofuata itawekwa nyuma kutoka kwenye ukingo sentimita 50 kuzunguka, na kimo cha mita 2. Sehemu itakayofuata nayo itawekwa nyuma ya ukingo sentimita 50 kuzunguka. Sehemu hii ya juu, ambayo itatumika kuteketezea sadaka, itakuwa mraba, kila upande mita 2. Mjengo wa kona za sehemu hii ya juu zitainuka kuliko sehemu nyingine. Sehemu ya juu ya madhabahu itakuwa mraba, mita 6 kila upande. Sehemu ya katikati, itakuwa mraba, sentimita 7 kila upande, nayo itakuwa na ukingo pembeni wenye kimo cha sentimita 25. Kutakuwa na mfereji wenye upana wa sentimita 50. Na kutakuwa na vidato vya kupandia madhabahu upande wa mashariki. Bwana Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Wewe mtu! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wakati madhabahu imejengwa, utaiweka wakfu kwa kutoa tambiko za kuteketezwa juu yake na kuinyunyizia damu ya wanyama waliotolewa sadaka. Wale makuhani walio wa kabila la Lawi ambao ni wazawa wa Sadoki, ndio tu watakaonikaribia ili kunihudumia. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Utawapa fahali mchanga kuwa sadaka ya kuondoa dhambi. Utatwaa damu yake na kuitia juu ya pembe nne za madhabahu na juu ya ncha nne za daraja na juu ya pambizo yake pande zote. Hivyo ndivyo utakavyoitakasa madhabahu na kuiweka wakfu. Utachukua pia fahali wa sadaka ya kuondoa dhambi; watamteketeza katika mahali palipochaguliwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, lakini nje ya mahali patakatifu. Kesho yake, utatoa beberu asiye na dosari, kuwa sadaka ya kuondoa dhambi; madhabahu itatakaswa kama ilivyotakaswa kwa damu ya fahali. Utakapokwisha kuitakasa, utatwaa fahali mdogo asiye na dosari na kondoo dume mmoja asiye na dosari na kuwaleta mbele yangu. Makuhani watawapaka chumvi na kuwatoa kuwa tambiko ya kuteketezwa, kwa Mwenyezi-Mungu. Kwa muda wa siku saba, kila siku utatambika beberu mmoja awe sadaka ya kuondoa dhambi. Pia watatoa fahali mmoja na kondoo dume mmoja asiye na dosari. Hivyo kwa muda wa siku saba, utafanya upatanisho na kuitakasa, na hivyo kuiweka wakfu madhabahu. Baada ya siku hizo saba, tokea siku ya nane na kuendelea, makuhani watatoa sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani. Nami nitawakubali. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Yule mtu akanirudisha kwenye lango la nje linaloelekea mashariki, nje ya patakatifu, nalo lilikuwa limefungwa. Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Lango hili litaendelea kufungwa. Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kulitumia, kwa sababu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nimeingia kupitia lango hilo. Hivyo litadumu likiwa limefungwa. Hata hivyo, mkuu anayetawala anaweza kwenda huko na kula chakula chake kitakatifu mbele yangu. Ni lazima aingie na kutokea lango la chumba cha kuingilia.” Yule mtu akanipeleka mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kwa njia ya lango la kaskazini. Nilipoangalia, nikaona utukufu wa Mwenyezi-Mungu umeijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hapo nikaanguka kifudifudi. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Wewe mtu! Tia maanani mambo yote unayoona na kusikia. Nitakueleza kanuni na masharti ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Zingatia moyoni mwako kwa makini, ni watu gani wanaoruhusiwa kuingia na kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ni watu gani wamekatazwa kuingia humo. Utawaambia hao watu waasi wa Israeli, Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: Siwezi kuendelea kuyavumilia machukizo yenu yote. Mmeitia unajisi maskani yangu kwa kuruhusu waingie humo watu wasiotahiriwa, watu wasionitii mimi, wakati mafuta na damu vinatambikwa kwa ajili yangu. Hivyo, nyinyi watu wangu mmelivunja agano langu kwa machukizo yenu yote. Badala ya kutekeleza huduma ya vitu vyangu vitakatifu, mmeruhusu watu wa mataifa mengine kutekeleza huduma hiyo katika maskani yangu. Sasa, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hakuna mtu yeyote wa taifa geni, asiyetahiriwa au asiyenitii mimi, atakayeruhusiwa kuingia maskani yangu; hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli, hawataruhusiwa. “Walawi walioniacha wakati ule Waisraeli walipojitenga nami kwa kufuata miungu yao, watabeba adhabu yao. Wataweza tu kuhudumu katika maskani yangu kama watumishi wakilinda malango ya nyumba yangu, na kutumikia katika nyumba. Wataweza kuchinja wanyama wanaotolewa na watu kwa ajili ya tambiko za kuteketeza na kuwatumikia watu. Lakini kwa sababu waliongoza ibada za miungu kwa ajili ya watu wa Israeli, wakawafanya watu kutenda dhambi, basi, nimeunyosha mkono wangu kuwaadhibu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Nao watabeba adhabu yao. Hawatanikaribia tena kunihudumia kama makuhani, wala hawatavigusa tena vitu vitakatifu wala vile vitakatifu kabisa. Bali wataaibika kwa sababu ya machukizo yao waliyotenda. Hata hivyo, watashika zamu ya kulinda nyumba, wakifanya huduma yote na kazi zote zitakazotendeka humo. “Lakini makuhani wa kabila la Lawi ambao ni wazawa wa Sadoki walioendeleza kazi yangu katika patakatifu pangu, wakati Waisraeli waliponiacha, hao ndio watakaoendelea kunitumikia na kuja mbele yangu kunitolea mafuta na damu. Hao tu ndio watakaoingia katika maskani yangu, nao watakaribia kwenye madhabahu kunitumikia. Lakini wanapoingia katika ua wa ndani, watavaa mavazi ya kitani; hawatavaa mavazi ya sufu watakapohudumu katika malango ya ua wa ndani na kwenye nyumba. Watavaa vilemba vya kitani vichwani mwao, na suruali za kitani viunoni mwao; lakini bila mkanda wowote. Watakapotoka kwenda kwenye ua wa nje kwa watu, watavua mavazi waliyovaa wakati walipokuwa wanahudumu na kuyaweka katika vyumba vitakatifu. Ni lazima wavae mavazi mengine, ili watu wasije wakawa najisi kwa kugusa mavazi yao. “Hawatanyoa vichwa vyao wala kuacha nywele zao ziwe ndefu. Lakini watapunguza tu mashungi ya nywele zao. Kuhani yeyote asinywe divai anapoingia ua wa ndani. Kuhani yeyote asioe mwanamke mjane wala mwanamke aliyepewa talaka. Lakini atamwoa bikira ambaye ni mzawa wa Waisraeli au mwanamke aliyefiwa na mumewe aliyekuwa kuhani. Makuhani watafundisha taifa langu kupambanua vitu vilivyo vitakatifu na visivyo vitakatifu, na kuwajulisha tofauti baina ya vitu vilivyo najisi na visivyo najisi. Kukiwako ugomvi wataamua kadiri ya sheria zangu. Katika sikukuu zote watafuata amri zangu na sheria zangu, na kuzitakasa sabato zangu. Hawatakaribia maiti ili wasijitie unajisi. Lakini wataweza kujitia unajisi kwa kumkaribia baba au mama au mtoto wa kike au wa kiume au dada yao asiyeolewa, aliyekufa. Mmoja wao akisha jitia unajisi, atakaa hali hiyo kwa muda wa siku saba. Kisha atakuwa safi. Siku atakapoingia katika patakatifu, katika ua wa ndani ili kuhudumu, atatoa sadaka yake ya kuondoa dhambi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Makuhani hawatakuwa na haki ya kumiliki ardhi; haki yao ni kunitumikia mimi. Hamtawapa milki katika nchi ya Israeli, watakachokuwa nacho ni mimi tu. Watakula sadaka ya nafaka, sadaka ya kuondoa dhambi, na sadaka ya kuondoa hatia. Kila kitu katika Israeli kilichowekwa wakfu kwa Mungu kitakuwa chao. Vitu vyote vilivyo bora vya malimbuko yenu na vya matoleo yenu ya kila aina vitakuwa kwa ajili ya makuhani. Tena mtawapa sehemu ya kwanza ya unga wenu, ili mlete baraka juu ya nyumba zenu. Makuhani hawatakula nyama ya mnyama au ndege yeyote aliyekufa mwenyewe au aliyeraruliwa na mnyama wa porini. “Mtakapoigawanya nchi kwa kura ili kila kabila lipate sehemu yake, sehemu moja ya nchi ni lazima iwekwe wakfu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu. Urefu wake utakuwa kilomita kumi na mbili u nusu na upana wa kilomita kumi. Eneo hilo lote litakuwa takatifu. Ndani yake kutakuwa na eneo mraba kwa ajili ya patakatifu, kila upande mita 250, na litazungukwa na eneo wazi lenye upana wa mita 250. Katika eneo hilo utapima pia sehemu yenye urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kwa kilomita tano; humo kutakuwa maskani yangu, mahali patakatifu kabisa. Eneo hilo litakuwa takatifu nchini, na kutengwa kwa ajili ya makuhani wanaomtumikia Mwenyezi-Mungu katika maskani yake. Ndani ya eneo hilo kutakuwa na nyumba zao na nafasi iliyowekwa wakfu kwa ajili ya maskani yangu. Eneo lingine lenye urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kwa kilomita tano, litatengwa kwa ajili ya miji ya Walawi wanaohudumu hekaluni liwe milki yao. “Mtapima eneo la mji karibu na eneo takatifu, lenye urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kwa kilomita mbili u nusu. Hilo litakuwa kwa ajili ya mtu yeyote wa Israeli. “Mtawala, naye atapewa eneo lake upande wa mashariki na magharibi wa eneo lililowekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Eneo hilo litaenea magharibi mpaka bahari ya Mediteranea na upande wa mashariki hadi mpaka wa mashariki wa nchi. Litakuwa na urefu sawa na eneo lililopewa kila kabila la Israeli. Hiyo ndiyo milki ya mtawala katika Israeli. Hivyo mtawala hatawadhulumu watu wangu, bali ataacha nchi igawiwe Waisraeli kulingana na makabila ya Israeli. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nyinyi watawala wa Israeli, mmefanya dhambi vyakutosha. Acheni ukatili na dhuluma. Tendeni mambo ya haki na sawa. Acheni kuwafukuza watu wangu nchini; mimi Bwana Mungu nimesema. Kila mtu ni lazima atumie mizani na vipimo halali. Kwa kipimo cha ulinganifu: Efa kwa nafaka na bathi kwa mafuta zina kiasi sawa. Hivyo viwili ni moja ya kumi ya homeri moja. Kwa kupimia uzani: Gera 20 ni shekeli moja, shekeli 50 ni mina moja. “Vipimo vya matoleo yenu ya nafaka vitakuwa hivi: Moja ya sita ya efa katika homeri moja ya ngano, na moja ya sita ya efa katika homeri moja ya shayiri. Kiwango cha mafuta kitakuwa hivi: Moja ya bathi ya mafuta kutoka kila kori (kori moja ni sawa na homeri moja ambayo ni sawa na bathi kumi). Watatoa kondoo mmoja kwa kila kundi la kondoo 200 katika jamaa za Israeli. Wataleta sadaka za nafaka, sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, ili wapate kufanyiwa upatanisho. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Watu wote nchini watampa sadaka hizo mtawala wa Israeli. Itakuwa ni wajibu wa mtawala kuhakikisha kuwa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zinazotolewa wakati wa sikukuu, mwezi mwandamo, sabato, na sikukuu zozote zilizowekwa zinapatikana kwa Waisraeli. Mtawala mwenyewe ataandaa sadaka za kuondoa dhambi, sadaka za nafaka, sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani ili kuwafanyia upatanisho watu wote wa Israeli. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, mtatambika fahali mdogo asiye na dosari ili kutakasa maskani yangu. Kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuipaka miimo ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kona za madhabahu, na miimo ya nafasi ya kuingilia kwenye ua wa ndani. Atafanya vivyo hivyo siku ya saba ya mwezi huo, kwa ajili ya kila mtu aliyetenda dhambi bila kukusudia au kwa kutojua. Kwa njia hiyo mtaitakasa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. “Siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, mtaadhimisha sikukuu ya Pasaka. Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Siku hiyo, mtawala atatoa fahali mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote wa Israeli. Kila siku, katika muda huo wa siku saba, atamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu fahali saba na kondoo madume saba wasio na dosari kwa kuwateketeza wazima. Tena ni lazima atoe sadaka kila siku ikiwa ni sadaka ya kuondoa dhambi. Kisha atatengeneza sadaka ya unga kilo 10 kwa kila fahali na kilo 10 kwa kila kondoo dume, halafu lita 3 za mafuta kwa kila kilo 10 za unga. “Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, na kwa muda wa siku saba za sikukuu, mtawala atatoa mahitaji kwa ajili ya sadaka za kuondoa dhambi, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Lango la ua wa ndani unaoelekea mashariki litafungwa siku zote sita za kazi. Siku za sabato na siku za mwezi mwandamo litafunguliwa. Toka nje, mtawala ataingia ukumbi wa ndani kwa kupitia lango la ukumbi huo. Naye atasimama karibu na nguzo ya lango, wakati makuhani wanateketeza sadaka zake za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha mtawala huyo atasujudia kwenye lango na baadaye atatoka nje. Lango litabaki wazi hadi jioni. Kila siku ya sabato na sikukuu ya mwezi mwandamo, watu wote wataniabudu mimi Mwenyezi-Mungu mbele ya lango. Siku ya sabato, mtawala atamletea Mwenyezi-Mungu wanakondoo sita na kondoo dume mmoja, wote wasio na dosari, kama sadaka ya kuteketezwa nzima. Pamoja na kila kondoo dume, ataleta sadaka ya unga lita kumi na saba na nusu, lakini pamoja na kila mwanakondoo ataleta sadaka yoyote anayoweza. Na kwa kila sadaka ya unga, ataleta lita tatu za mafuta. Wakati wa sikukuu ya mwezi mwandamo atatoa fahali mchanga, wanakondoo sita, na kondoo dume mmoja; wote wasio na dosari. Pamoja na kila fahali na kila kondoo dume anayetolewa sadaka, ni lazima pawepo lita kumi na saba na nusu za unga, na pamoja na kila mwanakondoo, ni lazima pawepo chochote ambacho mtawala anatoa. Tena kwa kila sadaka ya nafaka, ni lazima kutoa lita tatu za nafaka. “Mtawala anapotoka ni lazima auache ukumbi kwa njia ileile aliyoingia nayo. Watu wanapokuja kumwabudu Mwenyezi-Mungu wakati wa sikukuu yoyote, wale walioingia kwa njia ya lango la kaskazini, watatoka kwa njia ya lango la kusini; na wale walioingia kwa lango la kusini, watatoka kwa njia ya lango la kaskazini. Mtu asirudi kwa njia ya lango aliloingilia, bali atatoka kwa njia ya lango lililo mbele yake. Mtawala ataingia ndani watu wanapoingia, na atatoka wanapotoka. Wakati wa siku za sikukuu na siku zilizopangwa, sadaka za nafaka zitakuwa lita kumi na saba zikiandamana na kila fahali au kondoo dume, na chochote ambacho anayeabudu anaweza kutoa kwa kila mwanakondoo. Kwa kila sadaka ya nafaka atatoa lita tatu za mafuta. Mtawala anapotaka kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kwa hiari, iwe sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya amani, watamfungulia lango la ukumbi wa ndani unaoelekea mashariki. Atatoa sadaka kama anavyofanya siku ya sabato, na anapotoka, lango lifungwe nyuma yake. “Kila siku asubuhi mtamtolea Mwenyezi-Mungu mwanakondoo wa mwaka mmoja asiye na dosari, ambaye atateketezwa mzima. Pia kila siku, sadaka ya kilo mbili za unga itatolewa asubuhi pamoja na lita moja ya mafuta ya zeituni yakichanganywa na unga. Ni lazima kufuata sheria za sadaka hii kwa Mwenyezi-Mungu milele. Mwanakondoo, unga na mafuta ni lazima vitolewe kila siku asubuhi kwa Mwenyezi-Mungu milele. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ikiwa mtawala anampa mmojawapo wa wanawe zawadi ya ardhi, zawadi hiyo itakuwa mali ya huyo kijana milele kama sehemu ya jamaa yake. Lakini ikiwa atampa mmoja wa watumishi wake sehemu yoyote ya ardhi yake, zawadi hiyo itakuwa mali yake mpaka mwaka wa kuachwa huru. Ndipo itakapomrudia mtawala. Ni yeye tu na watoto wake wa kiume wanaoweza kuimiliki daima. Mtawala kamwe asipore mali ya watu. Ardhi yoyote anayowapa watoto wake wa kiume ni lazima itokane na eneo lake mwenyewe. Hivyo hatawadhulumu watu wangu kwa kuwanyanganya ardhi yao.” Kisha, yule mtu akanipitisha kwenye nafasi ya kupitia kuingia kwenye vyumba vitakatifu vya makuhani vinavyoelekea kaskazini, karibu na lango la kusini la ukumbi wa ndani. Akanionesha mahali, upande wa magharibi wa vyumba, akaniambia: “Hapa makuhani huchemsha nyama ya sadaka ya kuondoa hatia, sadaka ya kuondoa dhambi, na kuoka sadaka za nafaka. Kwa hiyo hawatoki nje ya ukumbi na chochote, ili watu wasije wakawa najisi kwa kugusa kitu kitakatifu.” Kisha akanipeleka kwenye uwanja wa nje, akanipitisha karibu na pembe nne za ua; kwa kila pembe ya ua kulikuwapo kiwanja kidogo, yaani, kwa pembe nne za ua vilikuwapo viwanja vinne vidogo vya urefu wa mita 20 na upana mita 15. Ulikuwapo ukuta kukizunguka kila kiwanja, na mahali pa moto mkabala na ukuta. Yule mtu akaniambia: “Haya ni majiko ambako watumishi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu watachemsha sadaka wanazoleta watu.” Yule mtu akanirudisha kwenye kiingilio cha hekalu. Huko, maji yalikuwa yakitoka chini ya kizingiti cha hekalu kuelekea upande wa mashariki, (kwa maana hekalu lilielekea mashariki). Maji yalikuwa yakitiririka kutoka chini ya upande wa kusini wa lango la hekalu, kusini mwa madhabahu. Kisha akanipeleka nje kwa njia ya lango la kaskazini. Akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, upande wa mashariki; na maji yalikuwa yanatoka upande wa kusini. Yule mtu, kwa ufito wake wa kupimia, akapima mita 500 kwenda chini upande wa mashariki, akanipitisha kwenye maji. Maji yalifika kwenye nyayo tu. Kisha akapima tena mita 500, akaniongoza kuvuka maji. Maji yakafika mpaka magoti yangu. Akapima tena mita nyingine 500, naye akaniongoza kuvuka maji. Maji yakafika mpaka kiunoni mwangu. Akapima mita 500 nyingine, na mto ukawa na kilindi kirefu hata sikuweza kuuvuka tena. Haikuwezekana kuuvuka ila kwa kuogelea. Yule mtu akaniambia, “Wewe mtu! Zingatia mambo hayo yote kwa makini.” Kisha, akanirudisha mpaka ukingo wa mto. Nilipofika huko niliona miti mingi sana kwenye kingo za mto. Akaniambia, “Maji haya yanatiririka kupitia nchini hadi Araba; na yakifika huko yatayafanya maji ya Bahari ya Chumvi kuwa maji mazuri. Kila mahali mto huu utakapopita, kutaishi aina zote za wanyama na samaki. Mto huu utayafanya maji ya Bahari ya Chumvi kuwa maji baridi. Kokote utakakopita utaleta uhai. Wavuvi watasimama ufuoni mwa bahari, na eneo kutoka Engedi mpaka En-eglaimu litakuwa la kuanikia nyavu zao. Kutakuwa na aina nyingi za samaki kama zilivyo katika Bahari ya Mediteranea. Lakini sehemu zake zenye majimaji na mabwawa kando ya bahari, hazitakuwa na maji mazuri. Bali hayo yatabaki kuwa maji ya chumvi. Kisha ukingoni mwa mto huo kutaota kila namna ya miti itoayo chakula. Majani yake hayatanyauka wala miti hiyo haitaacha kuzaa matunda. Itazaa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu inapata maji yanayotiririka kutoka maskani ya Mungu. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatatumika kuponya magonjwa.” Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Hii ndiyo mipaka ya nchi mtakayoyagawia makabila kumi na mawili ya Israeli. Lakini kabila la Yosefu lipewe maradufu. Nyote mtagawana sawa. Niliapa kuwa nitawapa wazee wenu nchi hii, nayo itakuwa mali yenu. Upande wa kaskazini mpaka utapita kutoka Bahari ya Mediteranea, kuelekea mji wa Hethloni, hadi mahali pa kuingia Hamathi na kuendelea hadi Zedadi. Kutoka hapo utaendelea hadi Berotha na Sibraimu (ulio kati ya Damasko na Hamathi), hadi mji wa Haser-hatikoni ulio mpakani mwa Haurani. Hivyo mpaka utakwenda kutoka bahari ya Mediteranea kuelekea mashariki hadi mji wa Hasar-enoni ukipakana na maeneo ya Damasko na Hamathi kwa upande wa kaskazini. Upande wa mashariki, mpaka utakuwa mto wa Yordani unaoelekea kati ya Haurani na Damasko, Gileadi na nchi ya Israeli. Pia mpaka utapitia upande wa mashariki wa Bahari ya Chumvi hadi Tamari. Upande wa kusini, toka Tamari mpaka utaendelea hadi chemchemi ya Meriba-kadeshi. Kutoka Meriba-kadeshi mpaka utaelekea kusini-magharibi hadi Bahari ya Mediteranea ukipitia mashariki ya nchi ya Misri. Upande wa magharibi, mpaka ni Bahari ya Mediteranea na utapanda kaskazini hadi mahali pa kuingilia Hamathi. “Basi, mtagawanya nchi hii kati yenu kulingana na makabila ya Israeli. Mtaigawanya kuwa mali yenu. Wageni watakaokaa kati yenu na wamezaa watoto, pia wapewe sehemu ya nchi mnapoigawanya. Hao ni lazima watendewe kama raia halisi wa Israeli na wana haki ya kupiga kura ili kupata sehemu ya nchi pamoja na makabila ya Israeli. Kila mgeni anayekaa nanyi atapewa sehemu yake pamoja na watu wa kabila ambamo anaishi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Haya ndiyo majina ya makabila na sehemu zao: Kuanzia mpaka wa kaskazini kwenye barabara ya Hethloni hadi kuingia Hamathi hadi mji wa Hazar-enoni (ulioko mpakani mwa Damasko na Hamathi upande wa kaskazini na kuendelea kutoka mashariki hadi magharibi), eneo hilo litakuwa la kabila la Dani. Eneo linalopakana na la Dani, kutoka mashariki hadi magharibi litakuwa la Asheri. Kabila la Naftali, litapata eneo linalopakana na lile la Asheri, kutoka mashariki hadi magharibi. Baada ya eneo la kabila la Naftali, litafuata eneo la kabila la Manase, kutoka mashariki hadi magharibi. Eneo linalopakana na eneo la Manase, kutoka upande wa mashariki hadi magharibi, litakuwa la kabila la Efraimu. Eneo linalopakana na eneo la Efraimu, kutoka mashariki hadi magharibi, litakuwa la kabila la Reubeni. Eneo linalopakana na eneo la Reubeni, kutoka mashariki hadi magharibi litakuwa la kabila la Yuda. Baada ya eneo la kabila la Yuda, utatenga eneo lenye urefu wa kilomita 12 na upana kama huohuo, kutoka kaskazini hadi kusini, na urefu huohuo kutoka mashariki hadi magharibi, sawasawa na eneo la kabila lolote. Hapo katikati ya eneo hilo patakuwa na maskani ya Mungu. Eneo utakalotenga kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu litakuwa lenye urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kwa kilomita 10. Makuhani watakuwa na eneo lao katika eneo hilo. Eneo hilo litakuwa na urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kutoka mashariki hadi magharibi, na kilomita 5 kutoka kaskazini hadi kusini. Maskani ya Mungu itakuwa katikati ya eneo hilo. Eneo hilo litakuwa kwa ajili ya makuhani wa wazawa wa Sadoki, ambao walinitumikia kwa uaminifu na hawakuasi wakati Waisraeli walipoasi kama Walawi walivyofanya. Hilo litakuwa eneo lao maalumu kutoka katika eneo takatifu la nchi, eneo takatifu kabisa, litakalopakana na eneo la Walawi. Nao Walawi, eneo lao litakuwa kusini mwa eneo la makuhani. Eneo hilo litakuwa na urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kutoka mashariki hadi magharibi, na upana kilomita 5 kutokea kaskazini hadi kusini. Hakuna sehemu yoyote ya eneo hilo itakayouzwa au kutolewa kwa mtu yeyote, kwa sababu eneo hilo ni takatifu kwa Mwenyezi-Mungu; nalo ni bora kuliko yote nchini. Ile sehemu ya eneo maalumu iliyobaki, yenye urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu na upana kilomita 2.5, hilo ni kwa matumizi ya kawaida ya mji: Mahali pa kuishi na eneo la mashamba. Katikati yake kutakuwa na mji, nao utakuwa wa mraba, kila upande mita 2,250. Kuuzunguka mji, kutakuwa na eneo wazi lenye upana wa mita 125. Eneo ambalo litabaki baada ya kujengwa hekalu, kusini mwa mji, kilomita 5 kwa kilomita 2.5, upande wa mashariki, na kilomita 5 kwa kilomita 2.5 upande wa magharibi, litakuwa eneo la wakulima kwa wakazi wa mji. Wafanyakazi wa mjini wa kabila lolote la Israeli wanaweza kulima katika eneo hilo. Hivyo, eneo lote utakalotenga, yaani eneo takatifu pamoja na eneo la mji, litakuwa la mraba, kilomita kumi na mbili u nusu kila upande. Eneo linalosalia katika pande zote za eneo takatifu na eneo la mji, yaani lile eneo lenye eneo mraba likiwa na kilomita kumi na mbili u nusus kwa kila upande tokea mashariki hadi magharibi, mkabala na maeneo ya makabila, litakuwa la mtawala. Lile eneo takatifu ambamo maskani ya Mungu itakuwa katikati yake, na eneo la Walawi pamoja na lile eneo la mji, yatakuwa katikati ya eneo la mtawala. Eneo la mtawala litakuwa katika mpaka wa eneo la kabila la Yuda na eneo la kabila la Benyamini. Makabila yaliyobaki yatagawiwa maeneo yao hivi: Kabila la Benyamini litapewa eneo kutoka mashariki hadi magharibi. Eneo linalopakana na eneo la Benyamini kutoka upande wa mashariki kuelekea upande wa magharibi litakuwa la kabila la Simeoni. Eneo linalopakana na kabila la Simeoni kutoka upande wa mashariki kuelekea upande wa magharibi litakuwa eneo la kabila la Isakari. Eneo linalopakana na kabila la Isakari kutoka upande wa mashariki kuelekea upande wa magharibi, litakuwa eneo la kabila la Zebuluni. Eneo linalopakana na kabila la Zebuluni, kutoka mashariki kuelekea magharibi, litakuwa eneo la kabila la Gadi. Eneo linalopakana na kabila la Gadi kuelekea kusini, mpaka utatoka mji wa Tamari hadi kwenye chemchemi za Meriba-kadeshi na kupitia upande wa mashariki ya Misri hadi Bahari ya Mediteranea. Hilo ndilo eneo la makabila ya Israeli. Humo ndimo watapewa maeneo yao, kila kabila eneo lake. Bwana Mwenyezi-Mungu amesema. Mji wa Yerusalemu utakuwa na ukuta ambao utakuwa na malango haya ya kutokea na kuingia: Upande wa kaskazini urefu wa ukuta utakuwa mita 2,250. Upande huo wa kaskazini utakuwa na malango matatu: Lango la Reubeni, lango la Yuda na lango la Lawi. Ukuta wa Mashariki utakuwa na urefu wa mita 2,250. Upande huo utakuwa na malango matatu: Lango la Yosefu, lango la Benyamini na lango la Dani. Ukuta wa upande wa kusini utakuwa na urefu wa mita 2,250. Upande huo utakuwa na malango matatu: Lango la Simeoni, lango la Isakari na lango la Zebuluni. Ukuta wa upande wa magharibi utakuwa na urefu wa mita 2,250. Upande huo nao utakuwa na malango matatu: Lango la Gadi, lango la Asheri na lango la Naftali. Jumla ya urefu wa kuta zote nne utakuwa ni mita 9,000. Jina la mji kutokea sasa na kuendelea litakuwa: “Mwenyezi-Mungu Yupo Hapa.” Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Yehoyakimu wa Yuda, mfalme Nebukadneza wa Babuloni alikwenda Yerusalemu, akauzingira mji. Bwana akamwacha Yehoyakimu atiwe mikononi mwa mfalme Nebukadneza pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu. Basi mfalme Nebukadneza akachukua mateka na vyombo akavipeleka nchini Shinari, akaviweka katika hazina ya miungu yake. Mfalme Nebukadneza akamwamuru Ashpenazi, towashi wake mkuu, amchagulie baadhi ya vijana wa Israeli wa jamaa ya kifalme na ya watu mashuhuri. Mfalme alitaka vijana wasio na kasoro, wazuri kwa umbo, wenye uzoefu wa kila hekima, wenye akili na maarifa na wanaofaa kutoa huduma katika ikulu. Alitaka pia vijana hao wafundishwe kusoma na kuandika lugha ya Wakaldayo. Mfalme aliagiza vijana hao wapewe chakula bora ambacho yeye mwenyewe alikula na divai ambayo alikunywa. Vijana hao walitakiwa wapewe mafunzo kwa miaka mitatu, kisha wapelekwe kwa mfalme. Miongoni mwa vijana waliochaguliwa walikuwa Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, wote wa kabila la Yuda. Huyo towashi mkuu akawapa majina mengine; Danieli akamwita Belteshaza, Hanania akamwita Shadraki, Mishaeli akamwita Meshaki na Azaria akamwita Abednego. Lakini Danieli aliamua kutojitia unajisi kwa kula chakula bora cha mfalme na kunywa divai yake. Kwa hiyo, alimwomba towashi mkuu amruhusu asile vitu hivyo na kujitia unajisi. Basi, Mungu akamjalia Danieli kupendelewa na kuhurumiwa na Ashpenazi, towashi mkuu. Lakini, towashi mkuu akamwambia Danieli, “Nina hofu kwamba bwana wangu mfalme ambaye ametoa maagizo kuhusu chakula na vinywaji unavyopaswa kutumia, ataona kuwa afya yako si nzuri kama ya wenzako wa rika lako. Hivyo maisha yangu yatakuwa hatarini.” Hapo Danieli akamwendea mtumishi aliyewekwa na towashi mkuu kumlinda yeye na wenzake kina Hanania, Mishaeli na Azaria, akamwambia, “Tafadhali utujaribu, sisi watumishi wako kwa muda wa siku kumi kwa kutupa mboga za majani na maji. Kisha, tulinganishe sisi na hao vijana wengine wanaokula chakula cha mfalme, halafu utoe uamuzi wako kulingana na jinsi utakavyoona.” Mlinzi akakubaliana nao, akawajaribu kwa muda wa siku kumi. Baada ya siku hizo kumi, aliwaangalia akaona kuwa wale vijana waliokula mboga za majani walionekana wenye afya na nguvu kuliko wale wengine wote waliolishwa chakula cha kifalme. Basi, yule mlinzi akawaacha waendelee kula mboga za majani badala ya chakula cha fahari na divai. Mungu aliwajalia vijana hao wanne maarifa na ujuzi katika elimu na hekima. Zaidi ya hayo, alimjalia Danieli kipawa cha kufasiri maono na ndoto. Muda ulipotimia ambapo hao vijana wangepelekwa kwa mfalme kama alivyokuwa ameagiza, yule towashi mkuu akawapeleka vijana wote mbele ya Nebukadneza. Mfalme alipozungumza nao wote, hakuna walioonekana kuwa bora kama Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Basi, wakakubaliwa kumhudumia mfalme. Jambo lolote la hekima au maarifa ambalo mfalme aliwauliza alijionea mwenyewe kwamba vijana hao wanne walikuwa bora mara kumi kuliko waaguzi na wachawi wote katika utawala wake. Danieli alidumu katika huduma ya ikulu mpaka mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi. Mnamo mwaka wa pili wa utawala wake, mfalme Nebukadneza aliota ndoto, akawa na wasiwasi sana rohoni hata usingizi ukamtoweka. Basi, mfalme akaamuru waganga, walozi na wachawi wa Wakaldayo waletwe ili wamfasirie ndoto yake. Wote wakaja na kusimama mbele yake. Mfalme Nebukadneza akawaambia, “Niliota ndoto, nayo inanipa wasiwasi, nami nataka nijulishwe tafsiri yake.” Wale Wakaldayo wakamwambia mfalme kwa Kiaramu, “Uishi, ee mfalme! Tusimulie ndoto yako nasi watumishi wako tutakufasiria.” Mfalme akawaambia, “Nimetoa kauli yangu kamili: Ikiwa hamtanijulisha ndoto yenyewe na maana yake, mtangolewa viungo vyenu kimojakimoja, na nyumba zenu zitabomolewa. Lakini mkiniambia hiyo ndoto na maana yake, nitawapa zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi, nijulisheni ndoto hiyo na maana yake!” Wao wakamjibu mara ya pili, “Mfalme, tusimulie ndoto hiyo, nasi watumishi wako tutakufasiria.” Hapo mfalme akawakatiza kwa kusema, “Najua kweli kwamba mnajaribu kupoteza wakati kwa kuwa mnaona kwamba nilikwisha toa kauli yangu kamili, kwamba msiponijulisha ndoto hiyo, adhabu yenu ni moja. Mmepatana kunidanganyadanganya na kunilaghailaghai huku muda unapita. Niambieni ndoto hiyo, nami nitajua kuwa mnaweza kunijulisha maana yake.” Wale Wakaldayo wakamjibu: “Mfalme, hakuna mtu yeyote duniani awezaye kutimiza matakwa yako. Hakuna mfalme yeyote, hata awe mkuu na mwenye nguvu kiasi gani aliyepata kuwauliza waganga au walozi au Wakaldayo jambo kama hilo. Jambo unalouliza, ee mfalme, ni gumu. Hakuna mtu anayeweza kukufunulia isipokuwa miungu peke yake ambayo haikai miongoni mwa wanaadamu.” Kusikia hivyo, mfalme Nebukadneza alikasirika na kughadhibika sana, akaamuru wenye hekima wote wa Babuloni waangamizwe. Basi, tangazo likaenea kuwa wenye hekima wote wauawe; Danieli na wenzake, nao pia wakatafutwa ili wauawe. Basi, Danieli, kwa tahadhari na busara, alimwendea Arioko, mkuu wa kikosi cha walinzi wa mfalme na ambaye alipewa jukumu la kuwaua wenye hekima wa Babuloni, akamwuliza, “Kwa nini amri ya mfalme ni kali hivyo?” Hapo Arioko akamsimulia Danieli kisa chote. Ndipo Danieli alipomwendea mfalme na kumwomba ampe muda ili aweze kumjulisha mfalme maana ya ndoto yake. Kisha, Danieli akarudi nyumbani, akawajulisha wenzake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo. Aliwaambia wamwombe Mungu wa mbinguni awaonee huruma kuhusu fumbo hilo, ili wao wasiangamie pamoja na wenye hekima wengine wa Babuloni. Ndipo Danieli alipofunuliwa fumbo hilo usiku katika maono. Naye Danieli akamshukuru Mungu wa mbinguni, akasema, “Na litukuzwe milele na milele jina lake Mungu. Hekima na nguvu ni vyake. Hubadilisha nyakati na majira, huwaondoa na kuwatawaza wafalme. Wenye busara huwapa hekima, wenye maarifa huwaongezea ufahamu. Hufunua siri na mafumbo, ajua kilichoko gizani, mwanga wakaa kwake. Kwako, ee Mungu wa wazee wangu, natoa shukrani na kukusifu, maana umenipa hekima na nguvu, umetujulisha kile tulichokuomba, umetujulisha kile kisa cha mfalme.” Basi, Danieli akamwendea Arioko aliyekuwa ameteuliwa kuwaangamiza wenye hekima wa Babuloni, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babuloni, ila nipeleke mimi mbele ya mfalme, nami nitamweleza maana ya ndoto yake.” Basi, Arioko akampeleka Danieli mbele ya mfalme kwa haraka na kumwambia, “Nimempata mtu fulani miongoni mwa mateka wa Yuda anayeweza kukufasiria ndoto yako, ee mfalme.” Mfalme akamwuliza Danieli, ambaye pia aliitwa Belteshaza, “Je, unaweza kunijulisha ndoto niliyoota na maana yake?” Danieli akamjibu mfalme, “Hakuna wenye hekima, wachawi, waganga wala wanajimu wanaoweza kukujulisha fumbo hilo lako. Lakini, yuko Mungu mbinguni ambaye hufumbua mafumbo, naye amekujulisha, ee mfalme Nebukadneza, mambo yatakayotukia siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyokujia kichwani mwako ulipokuwa umelala ni haya: Kwako ee mfalme, ulipokuwa umelala kitandani mwako, yalikujia mawazo kuhusu mambo yatakayotukia baadaye; naye Mungu afumbuaye mafumbo, alikuonesha yale yatakayotukia. Lakini mimi sikufumbuliwa fumbo hili kwa sababu nina hekima kuliko wanaadamu wengine, bali ili wewe mfalme, upate kujulishwa maana ya ndoto yako na kujua mawazo yako. “Katika ndoto yako, ee mfalme, uliona sanamu kubwa, yenye nguvu na iliyongaa sana, imesimama mbele yako. Sanamu hiyo ilikuwa ya kutisha mno. Kichwa cha sanamu hiyo kilikuwa cha dhahabu safi, kifua chake na mikono yake vilikuwa vya fedha na tumbo lake na mapaja yake vilikuwa vya shaba. Miguu yake ilikuwa ya chuma na nyayo zake zilikuwa za mchanganyiko wa chuma na udongo wa mfinyanzi. Ukiwa bado unaangalia, jiwe lilingoka lenyewe, bila kuguswa, na kuipondaponda miguu ya shaba na udongo wa mfinyanzi ya ile sanamu, na kuivunja vipandevipande. Mara kile chuma, udongo wa mfinyanzi, shaba, fedha na dhahabu, vyote vikavunjika vipandevipande na kuwa kama makapi ya mahali pa kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperushia mbali kisibakie hata kipande kimoja. Lakini lile jiwe lililoivunja ile sanamu likageuka kuwa mlima mkubwa na kuijaza dunia yote. “Hiyo ndiyo ndoto yako, ee mfalme. Na sasa tutakupa maana yake. Wewe, ee mfalme, mfalme wa wafalme! Mungu amekupa ufalme, uwezo, nguvu na utukufu! Amekupa mamlaka juu ya wanaadamu wote, wanyama wa porini na ndege wote wa angani, kokote kule waliko. Wewe ndiwe kile kichwa cha dhahabu! Baada yako utafuata ufalme mwingine, lakini ufalme huo utakuwa dhaifu. Huu utafuatwa na ufalme wa tatu unaofananishwa na shaba; huo utaitawala dunia yote. Baada ya falme hizo, utafuata ufalme mwingine imara kama chuma. Na kama vile chuma kivunjavyo na kupondaponda vitu vyote, ndivyo ufalme huo utakavyovunjavunja na kusagilia mbali falme zilizotangulia. Uliona pia kuwa nyayo na vidole vya sanamu hiyo vilikuwa nusu udongo wa mfinyanzi na nusu chuma. Hii ina maana kwamba ufalme huo utagawanyika; lakini utakuwa na kiasi fulani cha nguvu za chuma kwa sababu kulikuwa na chuma kilichochanganyikana na udongo wa mfinyanzi. Kama ulivyoona, vidole vyake vya miguu vilikuwa nusu chuma na nusu udongo wa mfinyanzi, na hii inamaanisha kwamba ufalme huo utakuwa na nguvu kiasi fulani na udhaifu kiasi fulani. Hii inamaanisha kwamba watawala wa ufalme huo watachanganyikana kwa kuoana na watu wasio wa taifa lao, lakini hawatafaulu kuchanganyikana kama vile chuma kisivyoweza kuchanganyikana na udongo wa mfinyanzi. Wakati wa wafalme hao, Mungu wa mbinguni ataanzisha ufalme ambao kamwe hautaangamizwa. Watu wengine hawataushinda na kuutawala ufalme huo, bali ufalme huo utaziponda na kuzikomesha falme zilizotangulia, nao utadumu milele. Uliliona jiwe lililongoka lenyewe toka mlimani, bila kuguswa, na jinsi lilivyoivunja vipandevipande ile sanamu iliyotengenezwa kwa chuma, shaba, udongo wa mfinyanzi, fedha na dhahabu. Ee mfalme, Mungu Mkuu amekufunulia mambo yatakayotukia baadaye. Mimi nimekusimulia. Ndoto yako ni ya kweli na maana yake ni halisi.” Ndipo mfalme Nebukadneza alipoanguka kifudifudi na kumsujudia Danieli na kuamuru wamtolee Danieli tambiko na ubani. Mfalme akamwambia Danieli, “Hakika, Mungu wako ni Mungu wa miungu na Bwana wa wafalme, na ndiye afumbuaye mafumbo kwa sababu umefaulu kunifumbulia fumbo hili.” Kisha mfalme Nebukadneza akamtunukia Danieli heshima kubwa, akampa zawadi nyingi kubwakubwa, na kumfanya mtawala wa mkoa wote wa Babuloni, na mkuu wa wenye hekima wote wa Babuloni. Danieli akamwomba mfalme, naye mfalme akawaweka Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa wasimamizi wa mambo ya utawala ya mkoa wa Babuloni. Lakini Danieli akabakia katika jumba la mfalme. Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo mita ishirini na nane na upana mita tatu. Aliisimamisha katika sehemu tambarare ya Dura, mkoani Babuloni. Kisha mfalme akaamuru maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na maofisa wote wa mikoa wahudhurie sherehe ya kuzindua rasmi sanamu aliyoisimamisha. Basi, maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na maofisa wote wa mikoa wakakusanyika tayari kwa uzinduzi wa sanamu aliyosimamisha mfalme Nebukadneza. Mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote, mnaamriwa kwamba mkisikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, lazima mwiname chini na kuiabudu sanamu ya dhahabu aliyosimamisha mfalme Nebukadneza. Na yeyote ambaye hatainama chini na kuiabudu, atatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali.” Kwa hiyo, watu wote, mara waliposikia sauti za baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, walianguka kifudifudi na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo mfalme Nebukadneza aliisimamisha. Wakati huo, baadhi ya Wakaldayo wakajitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Walimwambia mfalme Nebukadneza, “Uishi, ee mfalme! Wewe, ee mfalme, ulitoa amri kuwa kila mtu anaposikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na kila aina ya muziki, ainame chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu. Na kwamba mtu yeyote asiyeinama chini na kuiabudu sanamu hiyo, atupwe ndani ya tanuri ya moto mkali. Sasa, kuna Wayahudi fulani uliowateua kushughulikia mambo ya utawala wa mkoa wa Babuloni, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego; watu hawa, ee mfalme, hawakuitii amri yako. Wanakataa kuitumikia miungu yako na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Hapo mfalme Nebukadneza, huku akiwaka hasira, akaamuru Shadraki, Meshaki na Abednego waletwe mbele yake. Nao wakawaleta mbele ya mfalme. Mfalme Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba wewe Shadraki, wewe Meshaki na wewe Abednego, hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi, mtakaposikia tena sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, je, mko tayari kuinama chini na kuiabudu sanamu niliyotengeneza? Kama mkikataa, mtatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali. Je, ni mungu gani anayeweza kuwaokoa mikononi mwangu?” Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, sisi hatuhitaji kukujibu kuhusu jambo hilo. Ikiwa ndivyo, Mungu wetu ambaye tunamtumikia aweza kutuokoa katika tanuri ya moto mkali; tena atatuokoa mikononi mwako, ee mfalme. Lakini, hata kama haitafanyika hivyo, ujue wazi, ee mfalme, kwamba sisi hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyosimamisha.” Hapo, mfalme Nebukadneza akawaka hasira, sura yake ikabadilika kwa chuki dhidi ya Shadraki, Meshaki na Abednego. Akaamuru mwako wa moto wa tanuri uongezwe mara saba kuliko kawaida yake. Akaamuru watu fulani wenye nguvu kabisa katika jeshi lake wawafunge Shadraki, Meshaki na Abednego na kuwatupa katika ile tanuri ya moto mkali. Basi, vijana hao wakafungwa hali wamevaa makoti yao, kanzu zao, kofia na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuri ya moto mkali. Kwa vile amri ya mfalme ilikuwa kali, ule moto ulikuwa umewashwa ukawa mkali sana, hata ndimi za moto zikawateketeza wale watu waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego. Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego, wakiwa wamefungwa, wakatumbukia katika ile tanuri ya moto mkali. Basi, mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hatukuwafunga watu watatu na kuwatupa motoni?” Nao wakamjibu mfalme, “Naam, mfalme! Ndivyo!” Kisha akauliza, “Lakini sasa mbona ninaona watu wanne wakitembeatembea humo motoni bila kufungwa na wala hawadhuriki, na mtu wa nne anaonekana kama mwana wa miungu?” Basi, mfalme Nebukadneza akaukaribia mlango wa tanuri ya moto mkali, akaita, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Mkuu, tokeni mje hapa!” Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka motoni. Maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa na washauri wa mfalme, wote wakakusanyika pamoja, wakaona ya kuwa ule moto haukuweza kuwaunguza hao watatu. Nywele zao hazikuungua, mavazi yao hayakuungua, wala hawakuwa na harufu yoyote ya moto. Basi, mfalme Nebukadneza akasema, “Na asifiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego kwa kuwa alimtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake ambao wanamtegemea. Wao walikataa kutii amri yangu ya kifalme, wakaitoa mhanga miili yao badala ya kuabudu mungu mwingine, ila Mungu wao peke yake. Kwa hiyo, naamuru kwamba watu wa kabila lolote, taifa lolote au lugha yoyote, watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, watangolewa viungo vyao kimojakimoja na nyumba zao zitabomolewa. Maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.” Basi, mfalme Nebukadneza akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika mkoa wa Babuloni. “Mimi mfalme Nebukadneza, nawaandikia watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote kote duniani. Nawatakieni amani tele! Nimeona vema kuwajulisha ishara na maajabu ambayo Mungu Mkuu amenionesha. Jinsi gani zilivyo kubwa ishara zake Mungu! Maajabu yake ni makuu mno! Ufalme wake ni ufalme wa milele; enzi yake yadumu kizazi hata kizazi. “Mimi, Nebukadneza, nilikuwa ninaishi raha mstarehe nyumbani kwangu na kufana katika ikulu yangu. Lakini nikaota ndoto iliyonitisha; nikiwa nimelala kitandani, mawazo na maono kichwani mwangu yaliniogopesha. Hivyo, nikaamuru wenye hekima wote wa Babuloni waletwe mbele yangu ili wanieleze maana ya ndoto hiyo. Ndipo waganga, walozi, Wakaldayo na wanajimu wakaletwa. Nikawasimulia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunieleza maana yake. Baadaye, akaja Danieli, anayeitwa pia Belteshaza, jina la mungu wangu, ambaye roho ya miungu mitakatifu imo ndani yake. Nami nikamsimulia ndoto yangu, nikasema: Ee Belteshaza, uliye mkuu wa waganga, nafahamu kuwa roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako, na kwamba hakuna fumbo lililo gumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu; niambie maana yake. “Nilipokuwa nimelala, niliona maono haya: Niliona mti mrefu sana katikati ya dunia. Mti uliendelea kukua, ukawa imara na kilele chake kikafika mbinguni. Uliweza kuonekana kutoka kila mahali duniani. Majani yake yalikuwa mazuri. Ulikuwa umejaa matunda, kiasi cha kuitosheleza dunia nzima. Wanyama wote wa porini walipata kivuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake. Viumbe vyote vilipata chakula kutoka mti huo. “Nilipokuwa nimelala kitandani, niliona maono: Mlinzi mtakatifu alishuka kutoka mbinguni. Akapaaza sauti akisema, ‘Kateni mti huu na kuyakatakata matawi yake. Pukuteni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na watoroke chini yake na ndege kutoka matawi yake. Lakini acheni kisiki chake na mizizi yake ardhini, kwenye majani mabichi ya kondeni kikiwa kimefungwa hapo kwa mnyororo wa chuma na shaba. Mwacheni mtu huyo aloweshwe kwa umande wa mbinguni; mwacheni aishi pamoja na wanyama wa porini na kula nyasi mbugani. Akili yake ya utu ibadilishwe, awe na akili ya mnyama kwa miaka saba. Hii ni hukumu iliyotangazwa na walinzi; ni uamuzi wa walio watakatifu, ili wanaadamu wote kila mahali wapate kutambua kuwa Mungu Mkuu anayo mamlaka juu ya falme zote za wanaadamu; yeye humpa ufalme mtu yeyote ampendaye, humfanya mfalme hata mtu duni wa mwisho.’ “Hii ndiyo ndoto niliyoota mimi Nebukadneza. Sasa, wewe Belteshaza, nieleze maana yake; kwani wenye hekima wote katika ufalme wangu hawawezi kuniambia maana yake; lakini wewe utaweza kwa kuwa roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako.” Hapo, Danieli, aliyeitwa pia Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akamwambia, “Belteshaza, ndoto hii, wala maana yake visikufadhaishe!” Belteshaza akamjibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii na maana yake ingewahusu adui zako! Mti uliouona ukiwa mkubwa na wenye nguvu, ambao matawi yake marefu yalifika mbinguni, nao ukionekana kutoka kila mahali duniani, majani yake yakiwa mazuri, na matunda yake mengi ya kulisha viumbe vyote, wanyama wa porini wakipata kivuli chini yake, na ndege wa angani wakikaa katika matawi yake, basi, ni wewe ee mfalme ambaye umekuwa mkubwa na mwenye nguvu. Ukuu wako umefika mpaka mbinguni, na ufalme wako umeenea mpaka miisho ya dunia. Kisha ukaona tena, ee mfalme, Mlinzi mtakatifu akishuka kutoka mbinguni, akaamuru: ‘Ukateni mti huu, mkauangamize. Lakini acheni kisiki chake na mizizi yake ardhini kwenye majani mabichi ya kondeni, kikiwa kimefungwa hapo kwa mnyororo wa chuma na shaba. Mwacheni mtu huyo aloweshwe kwa umande wa mbinguni; mwacheni aishi pamoja na wanyama wa porini kwa miaka saba.’ “Hii basi, bwana wangu, ndiyo maana ya ndoto yako, kadiri ya uamuzi wa Mungu Mkuu juu yako: Wewe utafukuzwa mbali na wanaadamu! Utaishi pamoja na wanyama wa porini, utakula majani kama ng'ombe; utalowa kwa umande wa mbinguni. Utakaa katika hali hiyo kwa miaka saba, na mwishowe utatambua kwamba Mungu Mkuu ndiye mwenye uwezo juu ya falme za wanaadamu, na humpa ufalme mtu yeyote amtakaye. Tena amri ile ya kukiacha kisiki na mizizi ya mti huo ardhini ina maana hii: Wewe utarudishiwa tena ufalme wako hapo utakapotambua kwamba Mungu wa mbinguni ndiye atawalaye. Kwa sababu hiyo, ee mfalme, sikiliza shauri langu. Achana na dhambi zako na maovu yako, utende haki na kuwaonea huruma waliodhulumiwa; huenda muda wako wa fanaka ukarefushwa!” Hayo yote yalimpata mfalme Nebukadneza. Miezi kumi na miwili baadaye, mfalme Nebukadneza alikuwa anatembea juu ya dari ya ikulu ya mji wa Babuloni. Basi, akasema kwa sauti, “Tazama Babuloni, mji mkuu nilioujenga kwa nguvu zangu uwe makao yangu ya kifalme na kwa ajili ya utukufu wangu!” Mara tu alipotamka maneno hayo, sauti kutoka mbinguni ikatamka: “Ewe mfalme Nebukadneza, sikiliza ujumbe huu juu yako! Ufalme umekutoka! Utafukuzwa mbali na wanaadamu! Utaishi pamoja na wanyama wa porini kondeni, na utakula majani kama ng'ombe! Utakaa katika hali hiyo kwa muda wa miaka saba, na mwishowe utatambua kwamba Mungu Mkuu ndiye mwenye uwezo juu ya falme za wanaadamu, na humpa ufalme mtu yeyote amtakaye.” Mara moja jambo hilo juu ya mfalme Nebukadneza likatekelezwa. Alifukuzwa mbali na wanaadamu, akawa anakula majani kama ng'ombe. Alilowa kwa umande wa mbinguni, na nywele zake zikawa ndefu kama manyoya ya tai, na kucha zake kama za ndege. “Mwishoni mwa ile miaka saba, mimi Nebukadneza niliinua macho yangu kutazama juu mbinguni na akili zangu zikanirudia. Nilimshukuru Mungu Mkuu na kumheshimu yeye aishiye milele: Kwa sababu enzi yake ni enzi ya milele, ufalme wake wadumu kizazi hata kizazi. Wakazi wote wa dunia si kitu; hufanya atakavyo na viumbe vya mbinguni, na wakazi wa duniani; hakuna awezaye kumpinga, au kusema ‘Unafanya nini?’ “Wakati huo huo akili zangu zikanirudia; nilirudishiwa pia heshima yangu, fahari yangu na utukufu wa ufalme wangu. Washauri na maofisa wangu walikuja kunitafuta, nikarudishwa katika ufalme wangu na kupata heshima kama pale awali. “Na sasa, mimi Nebukadneza ninamsifu na kumtukuza na kumheshimu mfalme wa mbinguni. Maana matendo yake yote ni ya haki, naye huwashusha wenye kiburi.” Siku moja mfalme Belshaza aliwaandalia karamu kubwa maelfu ya wakuu wake na kunywa divai pamoja nao. Kutokana na kunywa divai, mfalme Belshaza akatoa amri vile vyombo vya dhahabu na fedha ambavyo mfalme Nebukadneza, baba yake, alivichukua kutoka hekalu la Yerusalemu, viletwe ili avitumie kunywea divai pamoja na maofisa wake, wake zake na masuria wake. Basi, vile vyombo vya dhahabu na fedha vilivyochukuliwa hekaluni Yerusalemu vikaletwa. Mfalme, maofisa wake, wake zake na masuria wake wakavitumia kunywea. Walikunywa huku wanaisifu miungu iliyotengenezwa kwa dhahabu, fedha, shaba, chuma, miti na mawe. Mara, vidole vya mkono wa mwanaadamu vikatokea na kuandika kwenye lipu ya ukuta wa ikulu ya mfalme, mahali palipomulikwa vizuri, mkabala na kinara cha taa. Mfalme aliuona mkono huo ukiandika. Basi, mfalme akabadilika rangi na fikira zake zikamfadhaisha, viungo vyake vikalegea na magoti yakaanza kutetemeka. Mfalme Belshaza akapaaza sauti waletwe wachawi, Wakaldayo wenye hekima na wanajimu waletwe. Walipoletwa, mfalme akawaambia wenye hekima hao wa Babuloni, “Yeyote atakayesoma maandishi haya na kunijulisha maana yake, atavishwa mavazi rasmi ya zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, na kupewa nafasi ya tatu katika ufalme.” Basi, wenye hekima wote wa mfalme wakaja, lakini hawakuweza kuyasoma maandishi hayo wala kumjulisha mfalme maana yake. Basi, mfalme Belshaza akazidi kuhangaika na rangi yake ikazidi kugeuka, nao wakuu wake wakawa na wasiwasi. Kutokana na kelele za mfalme na wakuu wake, mama mfalme aliingia ukumbini mwa karamu, akasema, “Uishi, ee mfalme! Si lazima mawazo yako yakufadhaishe na kubadilika rangi yako. Katika ufalme wako yupo mtu ambaye roho ya miungu mitakatifu imo ndani yake. Wakati wa utawala wa baba yako, mtu huyu alidhihirika kuwa mwenye ujuzi, ufahamu na hekima kama ya miungu. Baba yako, mfalme Nebukadneza, alimfanya kuwa mkuu wa waaguzi, wachawi, Wakaldayo wenye hekima, na wanajimu, kwa sababu ana roho njema, maarifa, ujuzi wa kufasiri ndoto, kufumbua mafumbo na kutatua matatizo. Jina la mtu huyo ni Danieli ambaye baba yako alimwita Belteshaza. Basi na aitwe, naye atakueleza maana ya maandishi haya.” Hapo, Danieli akaletwa mbele ya mfalme, naye mfalme akamwuliza: “Je, wewe ndiwe Danieli, mmoja wa mateka aliowaleta baba yangu mfalme, kutoka nchi ya Yuda? Nimesikia kwamba roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako, na kwamba una ujuzi, na akili, na hekima ya ajabu. Wenye hekima na wachawi walipoletwa hapa kusoma na kunieleza maana ya maandishi haya, walishindwa. Lakini, nimesikia kwamba wewe unaweza kueleza vitendawili na kutambua mafumbo. Basi, kama ukifaulu kusoma maandishi haya na kunieleza maana yake, utavishwa mavazi rasmi ya zambarau na kuvishwa mkufu wa dhahabu shingoni mwako. Utapewa nafasi ya tatu katika ufalme huu.” Danieli akamjibu mfalme Belshaza, “Waweza kukaa na zawadi zako ee mfalme au kumpa mtu mwingine. Hata hivyo, ee mfalme, nitakusomea maandishi hayo na kukueleza maana yake. Ee mfalme, Mungu Mkuu alimpa baba yako mfalme Nebukadneza, ufalme, ukuu, fahari na utukufu. Kwa sababu ya ukuu aliompa, watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote walitetemeka na kumwogopa. Nebukadneza aliweza kumuua mtu yeyote aliyetaka na kumwacha hai yeyote aliyetaka. Aliyetaka kumpandisha cheo alimpandisha, aliyetaka kumshusha cheo alimshusha. Lakini alipoanza kuwa na kiburi, akawa na roho ngumu na mwenye majivuno, aliondolewa katika kiti chake cha enzi, akanyanganywa utukufu wake. Alifukuzwa mbali na wanaadamu, akili yake ikafanywa kama ya mnyama, akaishi na pundamwitu, akawa anakula majani kama ng'ombe. Alinyeshewa mvua mwilini mpaka alipotambua kwamba Mungu Mkuu ndiye atawalaye falme za wanaadamu, naye humweka mfalme yeyote amtakaye. Lakini wewe Belshaza, mwanawe, ingawa unayajua haya yote, hukujinyenyekeza! Badala yake umejikuza mwenyewe dhidi ya Bwana wa mbinguni: Umeleta vyombo vya nyumba yake Mungu ukavitumia kunywea divai, wewe, maofisa wako, wake zako na masuria wako, na kuisifu miungu iliyotengenezwa kwa fedha, dhahabu, shaba, chuma, miti na mawe; miungu ambayo haioni, haisikii wala haijui lolote. Lakini Mungu, ambaye uhai wako u mkononi mwake, na njia zako zi wazi mbele yake, hukumheshimu! Basi, Mungu ametuma mkono uandike maandishi haya. “Maandishi yenyewe ni: ‘MENE, MENE, TEKELI, PARSINI.’ Na hii ndiyo maana yake: MENE maana yake, Mungu amehesabu siku za ufalme wako na kuukomesha. TEKELI maana yake, wewe umepimwa katika mizani, nawe ukaonekana huna uzito wowote. PERESI maana yake, ufalme wako umegawanywa kati ya Wamedi na Wapersi.” Hapo, mfalme Belshaza akaamuru Danieli avishwe mavazi rasmi ya zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni. Ikatangazwa kuwa Danieli atashikilia nafasi ya tatu katika ufalme. Usiku huo huo, mfalme Belshaza wa Wakaldayo, aliuawa; naye mfalme Dario, Mmedi, akashika utawala akiwa na umri wa miaka sitini na miwili. Mfalme Dario aliamua kuteua wakuu 120 kusimamia mambo ya utawala. Aliwateua pia wakuu watatu, Danieli akiwa mmojawapo, wawasimamie wale wakuu wengine na maslahi ya mfalme, asije akapata hasara. Muda si muda, Danieli akadhihirika kuwa bora kuliko wale wasimamizi wengine na wakuu wote kwa kuwa alikuwa na roho njema. Hivyo mfalme akanuia kumpa uongozi wa ufalme wote. Wale wakuu pamoja na maliwali wakatafuta kisingizio cha kumshtaki Danieli kuhusu mambo ya ufalme, lakini hawakuweza kupata sababu ya kumlaumu, wala kosa lolote, kwani Danieli alikuwa mwaminifu. Hakupatikana na kosa, wala hatia yoyote. Ndipo wakapatana hivi: “Hatutapata kisingizio chochote cha kumshtaki Danieli isipokuwa kama kisingizio hicho kitakuwa kinahusu sheria ya Mungu wake.” Basi, hao wakuu na maliwali kwa pamoja, wakamwendea mfalme na kumwambia, “Uishi ee mfalme Dario! Sisi wakuu uliotuweka, wasimamizi, maliwali, washauri na wakuu wa mikoa, sote tumepatana kuwa inafaa, ee mfalme, utoe amri na kuhakikisha inafuatwa kikamilifu. Amuru kwamba kwa muda wa siku thelathini kusiwe na mtu yeyote atakayeruhusiwa kuomba kitu chochote kwa mungu yeyote au kwa mtu yeyote, isipokuwa kutoka kwako wewe, ewe mfalme. Mtu yeyote atakayevunja sheria hii na atupwe katika pango la simba. Hivyo, ee mfalme Dario, utoe amri hiyo na kuitia hati sahihi yako ili isibadilishwe. Nayo itakuwa sheria ya Wamedi na Wapersi, sheria ambayo haibatilishwi.” Hivyo, mfalme Dario akaitia sahihi hati ya sheria hiyo. Danieli alipojua kuwa ile hati imetiwa sahihi, alirudi nyumbani kwake ghorofani katika chumba chake kilichokuwa na madirisha yaliyofunguka kuelekea Yerusalemu. Humo, Danieli, kama ilivyokuwa kawaida yake, alipiga magoti mara tatu kila siku akamwomba na kumshukuru Mungu wake. Watu wale waliofanya mpango dhidi ya Danieli waliingia ndani, wakamkuta Danieli akiomba dua na kumsihi Mungu wake. Basi, walikwenda kwa mfalme na kumshtaki Danieli kwa kutumia ile sheria, wakisema, “Mfalme Dario, je, hukutia sahihi hati ya sheria kuwa kwa muda wa siku thelathini hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuomba kitu chochote, kwa mungu yeyote, au kwa mtu yeyote isipokuwa kutoka kwako wewe, ee mfalme, na kwamba yeyote atakayevunja sheria hii atatumbukizwa katika pango la simba?” Mfalme akaitikia, “Hivyo ndivyo ilivyo, kulingana na sheria ya Wamedi na Wapersi ambayo haiwezi kubatilishwa.” Wakamwambia mfalme, “Yule Danieli aliye mmoja wa mateka kutoka nchi ya Yuda hakuheshimu wewe mfalme wala haitii amri uliyotia sahihi. Yeye anasali mara tatu kila siku.” Mfalme aliposikia maneno hayo, alisikitika sana. Akajitahidi sana kupata njia ya kumwokoa Danieli. Aliendelea kujaribu mpaka jua likatua. Wale watu wakamwendea mfalme Dario kwa pamoja na kumwambia, “Ee mfalme, ujue kuwa hakuna sheria wala amri yoyote ya Wamedi na Wapersi inayoweza kubatilishwa baada ya kuwekwa na mfalme.” Ndipo mfalme Dario akatoa amri, naye Danieli akaletwa na kutupwa katika pango la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako ambaye unamtumikia daima, na akuokoe.” Jiwe likaletwa na kuwekwa mlangoni mwa lile pango. Mfalme akalipiga mhuri wake binafsi na ule wa wakuu wake, ili uamuzi kuhusu Danieli usibatilishwe. Kisha mfalme akarudi katika ikuluni yake ambamo alikesha akifunga; hakufanya tafrija ya aina yoyote, na usingizi ukampaa. Alfajiri na mapema, mfalme Dario aliamka, akaenda kwa haraka kwenye pango la simba. Alipofika karibu akamwita Danieli kwa sauti ya huzuni, “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai! Je, Mungu wako unayemtumikia daima ameweza kukuokoa na simba hawa?” Danieli akamjibu mfalme, “Uishi, ee mfalme! Mungu wangu alileta malaika wake kuvifumba vinywa vya simba hawa, nao hawakunidhuru. Alifanya hivyo kwa sababu alijua mimi sina lawama yoyote kwake na wala sijafanya lolote baya mbele yako.” Hapo mfalme akafurahi sana; akaamuru Danieli atolewe pangoni. Basi wakamtoa, naye alikuwa hajadhurika hata kidogo, kwa sababu alimtegemea Mungu wake. Mfalme akaamuru wale watu waliomchongea Danieli wakamatwe, nao wakatupwa ndani ya lile pango la simba pamoja na wake zao na watoto wao. Nao, hata kabla hawajagusa chini, simba waliwashambulia na kuivunjavunja mifupa yao. Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa makabila yote, mataifa yote, na lugha zote duniani: “Nawatakieni amani kwa wingi. Nitatoa amri kwamba watu wote katika ufalme wangu ni lazima wamwogope na kumcha Mungu wa Danieli. “Yeye ni Mungu aliye hai, aishiye milele; ufalme wake kamwe hauwezi kuangamizwa, utawala wake hauna mwisho. Yeye hukomboa na kuokoa, hufanya ishara na maajabu mbinguni na duniani, maana amemwokoa Danieli makuchani mwa simba.” Basi, Danieli akapata fanaka wakati wa utawala wa mfalme Dario na wa mfalme Koreshi, Mpersi. Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wa mfalme Belshaza wa Babuloni, Danieli aliota ndoto na kuona maono akiwa amelala kitandani mwake. Aliiandika ndoto yake hii: “Mimi Danieli niliona katika maono usiku, pepo nne toka pande zote za mbinguni zikiichafua bahari kuu. Wanyama wakubwa wanne, wakainuka kutoka humo baharini, kila mmoja tofauti na mwenzake. Mnyama wa kwanza alikuwa kama simba, na alikuwa na mabawa kama ya tai. Nikiwa namwangalia, mabawa yake yalingolewa, naye akainuliwa na kusimama kwa miguu miwili kama binadamu. Kisha, akapewa akili ya binadamu. “Mnyama wa pili alikuwa kama dubu ambaye upande wake mmoja ulikuwa umeinuka. Kinywani mwake alikuwa na mbavu tatu alizozishikilia kwa meno yake. Sauti ikamwambia, ‘Haya, kula nyama nyingi kadiri uwezavyo.’ “Baada ya hayo, nilimwona mnyama mwingine. Huyu alikuwa kama chui mwenye mabawa manne ya ndege mgongoni mwake. Alikuwa na vichwa vinne na alipewa mamlaka. “Kisha, katika maono yangu hayo ya usiku nikamwona mnyama wa nne wa ajabu na wa kutisha, mwenye nguvu sana. Huyu alikuwa na meno makubwa ya chuma ambayo aliyatumia kula na kuvunjavunja, na mabaki aliyakanyagakanyaga kwa nyayo zake. Alikuwa tofauti na wale wanyama wengine watatu, kwani alikuwa na pembe kumi. Nilipokuwa naziangalia hizo pembe, niliona upembe mwingine mdogo ukiota miongoni mwa zile kumi. Ili kuupa nafasi upembe huu zile pembe nyingine tatu zilingolewa pamoja na mizizi yake. Ulikuwa na macho ya binadamu na kinywa kilichotamka maneno ya kujigamba. “Nikiwa bado naangalia, viti vya enzi viliwekwa hapo, kisha ‘Mzee wa kale na kale’ akaja, akaketi. Alikuwa amevaa vazi jeupe kama theluji; nywele zake zilikuwa kama sufu safi. Kiti chake cha enzi kilikuwa cha miali ya moto na magurudumu ya kiti chake yalikuwa ya moto uwakao. Kutoka kiti hicho kijito cha moto kilibubujika, kikatiririka. Maelfu walimtumikia, na mamilioni walisimama mbele yake. Mahakama ikawa tayari kwa kikao, na vitabu vikafunguliwa. “Kutokana na maneno ya kujigamba yaliyokuwa yanasemwa na ile pembe, nikatazama. Nikiwa natazama, huyo mnyama wa nne aliuawa, mwili wake ukaharibiwa na kutolewa uchomwe moto. Wale wanyama wengine walinyanganywa mamlaka yao, lakini wao wenyewe wakaachwa waendelee kuishi kwa muda fulani. “Wakati wa maono haya usiku, niliona mmoja kama mwana wa mtu akija katika mawingu, akamwendea yule ‘Mzee wa kale na kale,’ wakanileta mbele yake. Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme, ili watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote wamtumikie. Utawala wake ni wa milele na ufalme wake kamwe hautaangamizwa. “Maono niliyoyaona mimi Danieli yalinishtua, nami nikafadhaika. Nilimkaribia mmojawapo wa wale waliosimama huko na kumwuliza maana halisi ya mambo hayo yote. Naye akanisimulia na kunieleza maana yake: ‘Wanyama hao wanne wakubwa ni wafalme wanne watakaotokea duniani. Lakini watakatifu wa Mungu Mkuu watapewa ufalme, nao wataumiliki ufalme huo milele na milele.’ “Kisha nikataka nielezwe juu ya yule mnyama wa nne, ambaye alikuwa tofauti kabisa na wale wengine, wa ajabu na wa kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma na makucha yake ya shaba. Aliyatumia meno hayo kula na kuvunjavunja, na mabaki aliyakanyagakanyaga kwa nyayo zake. Aidha nilitaka nielezwe juu ya zile pembe kumi alizokuwa nazo kichwani mwake, na ule upembe mmoja ambao kabla haujaota, zilingoka pembe tatu; upembe uliokuwa na macho na kinywa ambacho kilitamka maneno ya kujigamba, na ambao ulionekana kuwa mkubwa kuliko pembe nyingine. “Nikiwa bado naangalia, pembe hiyo ilipigana vita na watakatifu, nayo ikawashinda. Lakini yule ‘Mzee wa kale na kale’ akainuka, akawapa haki watakatifu wa Mungu na wakati ulipotimia, hao watakatifu wakapewa ufalme. “Nikaelezwa hivi: ‘Yule mnyama wa nne ni ufalme wa nne utakaokuwako duniani. Ufalme huo utakuwa tofauti na falme nyingine, nao utaiangamiza dunia nzima. Utaibwaga chini na kuipasua vipandevipande. Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huo. Halafu watafuatwa na mfalme mwingine ambaye atakuwa tofauti na wale waliomtangulia, na atawaangusha wafalme watatu. Huyo atamkufuru Mungu Mkuu na kuwatesa watakatifu wake. Atajaribu kubadilisha nyakati na sheria zao, na watakatifu watatiwa mikononi mwake kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Lakini mahakama itafanya kikao; watamnyanganya utawala wake, nao utafutwa na kuangamizwa kabisa. Ufalme, utawala na ukuu wa falme zote duniani watapewa watu wa watakatifu wa Mungu Mkuu. Ufalme wao utakuwa wa kudumu milele, na tawala zote zitawatumikia na kuwatii.’ “Huu ndio mwisho wa jambo hilo. Mawazo yangu yalinishtua sana mimi Danieli, hata rangi yangu ikabadilika. Lakini nililiweka jambo hilo moyoni mwangu. “Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Belshaza, maono mengine yalinijia mimi Danieli, licha ya maono yale ya kwanza. Katika maono haya, nilijikuta niko Susa, mji mkuu wa mkoa wa Elamu. Nilikuwa nimesimama kando ya mto Ulai. Nilipoinua macho yangu, niliona kondoo dume amesimama kando ya mto huo. Kondoo huyo alikuwa na pembe mbili ndefu, lakini moja ilikuwa ndefu zaidi, nayo ilitokea baada ya ile nyingine. Nilimwona huyo kondoo dume akishambulia kuelekea magharibi, kaskazini na kusini. Hakuna mnyama yeyote aliyethubutu kusimama mbele yake, wala kuzikwepa nguvu zake. Alifanya apendavyo na kujikweza mwenyewe. “Nilipokuwa ninawaza juu ya jambo hili, niliona beberu mmoja kutoka upande wa magharibi akija kasi bila kugusa ardhi. Kati ya macho yake alikuwa na pembe moja kubwa sana. Alimwendea yule kondoo dume mwenye pembe mbili niliyemwona akiwa amesimama kando ya mto, akamshambulia kwa nguvu zake zote. Nilimwona akimsogelea yule kondoo dume. Alikuwa amemkasirikia sana yule kondoo dume, hivyo akamshambulia kwa nguvu na kuzivunja zile pembe zake mbili. Yule kondoo dume hakuweza kustahimili. Alibwagwa chini na kukanyagwakanyagwa, wala hapakuwa na yeyote wa kumwokoa katika nguvu zake. Hapo yule beberu alijikweza sana. Lakini alipofikia kilele cha nguvu zake, ile pembe yake kubwa ikavunjika. Badala yake zikaota pembe nne zilizoonekana waziwazi, zikiwa zimeelekea pande nne za pepo. “Katika mojawapo ya pembe hizo nne, paliota upembe mwingine mdogo, ukakua sana kuelekea upande wa kusini-mashariki, na kuelekea nchi ile nzuri mno. Upembe huo ulikua sana kufikia viumbe vya mbinguni; ukaziangusha chini baadhi ya nyota na kuzikanyagakanyaga. Upembe huo ukajikweza juu ya mkuu wa viumbe vya mbinguni. Ukakomesha tambiko za kuteketezwa ambazo mkuu wa viumbe vya mbinguni alitambikiwa kila siku, na kukufuru maskani yake. Viumbe vya mbinguni vikatiwa nguvuni mwake pamoja na tambiko za kuteketezwa kila siku, kwa njia ya upotovu. Nao ukweli ukatupwa chini. Upembe huo ukaibwaga chini ibada ya kweli. Ulifanikiwa katika kila jambo ulilofanya. “Kisha, nikamsikia mtakatifu mmoja akizungumza na mwenzake. Huyo mwenzake alimwuliza, ‘Je, matukio yaliyotangazwa na maono haya yataendelea kwa muda gani? Kwa muda gani sadaka za kuteketezwa za kila siku zitabaki zimebatilishwa? Kwa muda gani upotovu wa kuangamiza kila kitu utaendelea, na mahali patakatifu pamoja na viumbe vya mbingu vitaendelea kukanyagwa?’ Yule mtakatifu wa kwanza akamjibu, ‘Kwa muda wa nyakati za jioni na asubuhi 2,300. Kisha maskani ya Mungu itapata tena hali yake halisi.’ “Mimi Danieli nilipoyaona hayo maono, na nilipokuwa nikijaribu kujua maana yake, ghafla, mmoja kama mwanaadamu akasimama mbele yangu. Nikasikia sauti ya mwanaadamu kutoka katika mto Ulai ikiita, ‘Gabrieli, mweleze mtu huyu maana ya maono aliyoona.’ Gabrieli akaja karibu na mahali niliposimama. Mimi nikaogopa sana, hata nikaanguka kifudifudi. Lakini akaniambia, ‘Wewe mtu, elewa kwamba maono uliyoyaona yanahusu wakati wa mwisho.’ “Alipokuwa anazungumza nami, mimi nikashikwa na usingizi mzito huku nimelala kifudifudi. Lakini yeye akanishika na kunisimamisha. Kisha akaniambia, ‘Sikiliza, ninakufahamisha matokeo ya ghadhabu ya Mungu yatakavyokuwa. Maono hayo yanahusu wakati wa mwisho. “ ‘Yule kondoo dume uliyemwona mwenye pembe mbili, ni wafalme wa Media na Persia. Yule beberu ni mfalme wa Ugiriki. Ile pembe kubwa katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza. Ile pembe iliyovunjika na badala yake zikaota pembe nne, ina maana kwamba ufalme huo mmoja utagawanyika kuwa falme nne, lakini falme hizo hazitakuwa na nguvu kama ule ufalme wa kwanza. Wakati falme hizo zitakapofikia kikomo chake na uovu wao kufikia kilele chake, patatokea mfalme mmoja shupavu na mwerevu. Atakuwa mwenye mamlaka makubwa, atasababisha uharibifu mbaya sana, na atafanikiwa katika kila atendalo. Atawaangamiza watu maarufu na watakatifu wa Mungu. Kwa ujanja wake, atafanikiwa katika mipango yake ya hila, naye atajikweza. Atawaangamiza watu wengi bila taarifa, na atataka kupigana na Mkuu wa wakuu, lakini ataangamizwa pasipo kutumia nguvu za kibinadamu. Maono ya hizo nyakati za jioni na za asubuhi ambayo yameelezwa ni ya kweli. Lakini uyafiche, kwani ni siri, na bado utapita muda mrefu kabla hayajatimia.’ “Mimi Danieli, nikazimia na kuugua kwa muda. Nilipopona, nikaendelea na shughuli za mfalme. Lakini yale maono yalinistaajabisha, nami sikuweza kuyaelewa. “Katika mwaka Dario mwana wa Ahasuero, Mmedi, alipoanza kutawala juu ya milki ya Wakaldayo, mimi Danieli nilikuwa nikivisoma kwa makini vitabu vitakatifu, na humo nikaelewa maana ya jambo lile Mwenyezi-Mungu alilomfahamisha nabii Yeremia kuhusu ile miaka sabini, muda ambao utahusika na kuharibiwa kwa Yerusalemu. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, kwa moyo, nikimtolea dua pamoja na kufunga, nikavaa vazi la gunia na kuketi kwenye majivu. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, na kuungama, nikisema: “Ee Bwana, wewe ni Mungu mkuu na wa kuogofya. Wewe ni mwaminifu kwa agano lako na unawafadhili wakupendao na kuzitii amri zako. Tumetenda dhambi, tumekosa, tumetenda maovu na kukuasi. Tumezikiuka amri zako na kanuni zako. Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako waliongea na wafalme wetu, wakuu wetu, wazee wetu na taifa letu lote. Kwako, ee Bwana, kuna uadilifu, lakini sisi daima tumejaa aibu. Jambo hili ni kweli kwetu sote tuishio Yudea, wakazi wa mji wa Yerusalemu na Waisraeli wote ambao umewatawanya katika nchi za mbali na za karibu kwa sababu ya kukosa uaminifu kwako. Aibu, ee Bwana, ni juu yetu, wafalme wetu, wakuu wetu na wazee wetu, kwa sababu tumekukosea. Wewe, Bwana Mungu wetu, una huruma na msamaha, ingawa sisi tumekuasi. Tulikataa kukusikiliza, ee Bwana, Mungu wetu; hatukuishi kulingana na sheria zako ulizotupa kwa njia ya watumishi wako manabii. Waisraeli wote wameiasi sheria yako, wamekuacha wakakataa kukutii. Kwa sababu tumekukosea, tumemwagiwa laana na viapo vilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtumishi wako. Umethibitisha yale uliyosema utatutenda sisi pamoja na watawala wetu kwa kuuadhibu mji wa Yerusalemu vikali zaidi ya mji mwingine wowote duniani. Umetuadhibu kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, lakini mpaka sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, hatukuomba msamaha wako kwa kuziacha dhambi zetu na kutafakari uaminifu wako. Kwa hiyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ulikuwa tayari kutuadhibu, na ukafanya hivyo, kwa kuwa daima unafanya yaliyo ya haki, nasi hatukukusikiliza. “Na sasa ee Bwana, Mungu wetu, uliyewatoa watu wako nchini Misri kwa nguvu yako kuu na kulifanya jina lako litukuke mpaka sasa, tunasema kwamba tumetenda dhambi; tumefanya maovu. Ee Bwana, kwa kadiri ya matendo yako ya haki usiukasirikie wala kuughadhibikia mji wako wa Yerusalemu, mlima wako mtakatifu. Watu wote wa nchi za jirani wanaudharau mji wa Yerusalemu na watu wako, kwa sababu ya dhambi zetu na maovu waliyotenda wazee wetu. Kwa hiyo, ee Mungu, isikilize sala yangu na maombi yangu mimi mtumishi wako. Kwa hisani yako, uifadhili tena maskani yako iliyoharibiwa. Tega sikio, ee Mungu wangu; angalia uone taabu tulizo nazo na jinsi unavyotaabika huo mji uitwao kwa jina lako. Tunakutolea maombi yetu si kwa sababu tumetenda haki, bali kwa sababu wewe una huruma nyingi. Ee Mwenyezi-Mungu, utusikie; utusamehe ee Mwenyezi-Mungu. Ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako utusikie na kuchukua hatua, wala usikawie, ee Mungu wangu, kwa ajili ya mji huu na watu hawa wanaoitwa kwa jina lako! “Basi, nilipokuwa nikiomba, nikiungama dhambi zangu na dhambi za watu wangu wa Israeli, pamoja na kumsihi Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya mlima wake mtakatifu, yule mtu Gabrieli, ambaye nilikuwa nimemwona katika maono hapo awali, alishuka kwa haraka mpaka mahali nilipokuwa. Ilikuwa wakati wa kutoa sadaka ya jioni. Basi, akaniambia, ‘Danieli, nimekuja kukupa hekima na uwezo wa kufahamu. Ulipoanza kuomba, Mungu alitoa jibu, nami nimekuja kukueleza jibu hilo kwa kuwa unapendwa sana. Kwa hiyo, usikilize kwa makini jibu hilo na kuelewa maono hayo. “ ‘Muda wa miaka saba mara sabini umewekwa kwa ajili ya watu wako na juu ya mji wako mtakatifu ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, kusamehe uovu, kuleta haki ya milele, kutia mhuri maono na unabii na kupaka mafuta mahali patakatifu kabisa. Basi, ujue na kufahamu jambo hili: Tangu wakati itakapotolewa amri ya kujengwa upya mji wa Yerusalemu hadi kuja kwake aliyepakwa mafuta, yule aliye mkuu, ni muda wa majuma saba. Kwa muda wa majuma sitini na mawili, mji wa Yerusalemu utajengwa upya, wenye barabara kuu na mahandaki, lakini wakati huo utakuwa wa taabu. Baada ya majuma hayo sitini na mawili, yule aliyepakwa mafuta atakatiliwa mbali hatabaki na kitu. Mji na mahali patakatifu kabisa vitaharibiwa na jeshi la mtawala atakayekuja kushambulia. Mwisho wake utafika kama mafuriko, kukiwa na vita na maangamizi kama yalivyopangwa na Mungu. Mtawala huyo atafanya mapatano imara na watu wengi kwa muda wa miaka saba. Baada ya nusu ya muda huo atakomesha tambiko na sadaka. Mahali pa juu hekaluni patasimamishwa chukizo haribifu, nalo litabaki hapo mpaka yule aliyelisimamisha atakapoangamizwa kama ilivyopangwa na Mungu.’” Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Koreshi wa Persia, Danieli, aliyeitwa pia Belteshaza, alipewa ufunuo. Ufunuo huo ulikuwa wa kweli, lakini ulikuwa mgumu sana, haukueleweka. Hata hivyo alielewa ufunuo huo maana pia alifahamu maono. “Wakati huo, mimi Danieli, nilikuwa nikiomboleza kwa muda wa majuma matatu. Sikula chakula cha fahari, sikugusa nyama wala divai, na sikujipaka mafuta kwa muda wa majuma hayo yote matatu. “Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilikuwa nimesimama kando ya mto Tigri. Nikainua macho, nikamwona mtu amevaa mavazi ya kitani na kiunoni amejifunga mkanda wa dhahabu kutoka Ufazi. Mwili wake ulingaa kama zabarajadi safi. Uso wake ulifanana na umeme, na macho yake yaliwaka kama miali ya moto. Miguu na mikono yake ilingaa kama shaba iliyosuguliwa sana. Sauti yake ilivuma kama sauti ya umati mkubwa wa watu. “Mimi Danieli peke yangu niliona maono hayo. Wale watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona, lakini walishikwa na hofu sana, wakakimbia, wakajificha. Hivyo, niliachwa peke yangu nikiangalia hayo maono ya kushangaza. Nguvu zikaniishia, na rangi yangu ikaharibika, nikabaki bila nguvu. Nilipoisikia sauti yake, nilianguka chini kifudifudi, nikashikwa na usingizi mzito. Hapo, mkono ukanigusa, ukanisimamisha, na kuimarisha miguu na mikono yangu. Akaniambia, ‘Danieli, wewe unayependwa sana, simama wima usikilize kwa makini maneno nitakayosema, maana nimetumwa kwako.’ Alipokuwa akiniambia maneno haya, mimi nilisimama nikitetemeka. Ndipo yeye akaniambia, ‘Danieli, usiogope. Mungu alilisikia ombi lako tangu siku ile ya kwanza ulipoamua kujinyenyekesha mbele yake ili upate ufahamu. Mimi nimekuja kwa ajili ya ombi lako hilo. Mkuu wa ufalme wa Persia alinipinga kwa muda wa siku ishirini na moja. Lakini Mikaeli, mmoja wa wakuu, akaja kunisaidia, kwa hiyo nikamwacha huko pamoja na mkuu wa ufalme wa Persia, nami nimekuja kukusaidia uyafahamu mambo yatakayowapata watu wako wakati ujao, kwani maono uliyoona yanahusu wakati ujao.’ “Alipokuwa ananiambia maneno hayo, niliangalia chini bila kuweza kuongea. Kisha, mmoja mwenye umbo la binadamu, aliigusa midomo yangu, nami nilifungua midomo yangu na kumwambia huyo aliyesimama karibu nami, ‘Ee bwana, maono haya yameniletea maumivu makali hata nimeishiwa nguvu. Mimi ni kama mtumwa mbele ya bwana wake. Nawezaje kuzungumza nawe? Sina nguvu na pumzi imeniishia!’ “Yule mmoja aliyeonekana kama mwanaadamu akanigusa kwa mara nyingine, akanitia nguvu. Akaniambia, ‘Usiogope wewe unayependwa sana, uko salama. Uwe imara na hodari.’ Aliposema nami, nilipata nguvu, nikamwambia, ‘Bwana, umekwisha niimarisha; sema kile ulichotaka kusema.’ Naye akaniambia, ‘Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa ni lazima nirudi kupigana na malaika mlinzi wa Persia. Halafu, nitakapokuwa nimemshinda, malaika mlinzi wa mfalme wa Ugiriki atatokea. Lakini nitakujulisha yale yaliyoandikwa katika kitabu cha ukweli. Sina mwingine wa kunisaidia kuwashinda hawa isipokuwa Mikaeli, malaika mlinzi wenu. “ ‘Lakini kwa upande wangu mimi, katika mwaka wa kwanza wa mfalme Dario Mmedi, nilijitoa kumthibitisha na kumtia nguvu. Sasa nitakueleza ule ukweli wa mambo haya. “ ‘Tazama, wafalme wengine watatu wataitawala nchi ya Persia. Hao watafuatwa na mfalme wa nne ambaye atakuwa tajiri kuliko wale waliomtangulia. Wakati wa kilele cha nguvu na utajiri wake, ataanza kuushambulia ufalme wa Ugiriki. Kisha atatokea mfalme hodari atakayetawala eneo kubwa na kufanya atakavyopenda. Hata hivyo, wakati wa kilele cha uwezo wake, ufalme wake utavunjika na kugawanyika katika sehemu nne kuelekea pepo nne za mbingu. Wazawa wake hawatatawala, wala ufalme hautakuwa mikononi mwa milki aliyotawala, kwa sababu ufalme wake utachukuliwa na wengine. “ ‘Mfalme wa kusini atakuwa mwenye nguvu. Lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu kuliko yeye na utawala wake utakuwa mkubwa zaidi. Baada ya miaka kadhaa, watafanya mkataba; binti mfalme wa kusini ataolewa katika jamaa ya mfalme na kuratibisha huo mkataba; wa kaskazini, lakini hataendelea kuwa na nguvu, pia mfalme na wazawa wake hawatavumilia; na huyo binti, mwanawe na watumwa wa kike aliokwenda nao, wote watauawa. Baadaye, mmojawapo wa ukoo wa huyo binti atakuwa mfalme. Huyo atayashambulia majeshi ya mfalme wa kaskazini na kuingia katika ngome zao na kushinda. Atazibeba sanamu za kusubu za miungu yao na vyombo vya thamani vya fedha na dhahabu mpaka nchini Misri. Kwa muda wa miaka kadhaa, mfalme wa kusini hatamshambulia mfalme wa kaskazini. Lakini baadaye, mfalme huyu wa kaskazini atauvamia ufalme wa kusini, ila atalazimika kurudi katika nchi yake. “ ‘Wana wa mfalme wa kaskazini watakusanya jeshi kubwa na kujiandaa kwa vita. Jeshi hilo litasonga mbele kama mafuriko litapita na kupigana vita mpaka ngome ya adui. Hapo, mfalme wa kusini, kwa hasira yake, atapigana vita na mfalme wa kaskazini ambaye naye atamkabili kwa jeshi kubwa, lakini litashindwa. Baada ya kulishinda vibaya jeshi la kaskazini na kuua maelfu, ataanza kujisifu, ila hataendelea kuwa mshindi. “ ‘Maana mfalme wa kaskazini baadaye ataandaa jeshi kubwa kuliko lile la awali. Kisha baada ya miaka kadhaa atarudi na jeshi kubwa lenye vifaa vingi. Wakati huo watu wengi watamwasi mfalme wa kusini. Baadhi ya watu wakatili wa taifa lako Danieli, wataasi ili kutekeleza maono haya, lakini hawatafaulu. Ndipo mfalme wa kaskazini atauzingira mji wenye ngome imara na kuuteka. Wanajeshi wa kusini hawatastahimili, hata wale wateule, maana hawatakuwa na nguvu. Mvamizi atawatenda kama apendavyo, hakuna atakeyethubutu kupingana naye. Atasimama katika nchi tukufu, na nchi hiyo yote itakuwa chini ya mamlaka yake. “ ‘Huyo mvamizi atakusudia kuja na jeshi lake lote, naye atafanya mapatano na kuyatekeleza. Atamwoza binti mmoja ili kuuangamiza ufalme wa adui yake; lakini mpango wake hautafaulu, wala kumfaidia lolote. Baadaye, atazigeukia na kuzishambulia nchi nyingi za pwani na kuzishinda. Lakini jemadari mgeni atamshinda na kuyakomesha majivuno yake mwenyewe; naam, atamrudishia mfalme wa kaskazini majivuno yake mwenyewe. Hapo atageuka kurudi katika ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka vitani na huo ndio utakaokuwa mwisho wake. “ ‘Huyu atafuatwa na mfalme mwingine ambaye atatuma mtozaushuru kupitia katika fahari ya ufalme wake. Mfalme huyo atauawa baada ya siku chache, lakini si kwa hasira wala vitani. “ ‘Mfalme atakayefuata atakuwa baradhuli ambaye hana idhini ya kushika ufalme, naye atakuja bila taarifa na kunyakua ufalme kwa hila. Majeshi pamoja na kuhani wa hekalu, atawafagilia mbali na kuwaua. Kwa kufanya mapatano, atayahadaa mataifa mengine, na ataendelea kupata nguvu ingawa atatawala taifa dogo. Bila taarifa atazivamia sehemu za mkoa zenye utajiri mwingi na kufanya mambo ambayo hayakufanywa hata na mmoja wa wazee wake waliomtangulia. Kisha, atawagawia wafuasi wake mateka, mali na vitu alivyoteka nyara vitani. Atafanya mipango ya kuzishambulia ngome, lakini kwa muda tu. “ ‘Kwa ujasiri mwingi, ataunda jeshi kubwa ili kuushambulia ufalme wa kusini, naye mfalme wa kusini atajibu mashambulizi hayo kwa jeshi kubwa zaidi na lenye nguvu sana. Lakini, mfalme wa kusini hatafaulu kwani mipango ya hila itafanywa dhidi yake. Wale wanaokula pamoja naye, ndio watakaomwangamiza. Watamwangamiza na jeshi lake litafagiliwa mbali na wengi watauawa. Hapo wafalme hao wawili wataketi pamoja mezani kula, lakini kila mmoja anamwazia mwenzake uovu, na kudanganyana. Ila hawatafanikiwa, maana wakati uliopangwa utakuwa bado haujatimia. Mfalme wa kaskazini atarudi nchini mwake akiwa na mali nyingi, lakini nia yake moyoni ni kulitangua agano takatifu. Atafanya apendavyo, kisha atarudi katika nchi yake. “ ‘Katika wakati uliopangwa ataivamia nchi ya kusini kwa mara nyingine, lakini safari hii, mambo yatakuwa tofauti. Meli kutoka Kitimu zitamshambulia, naye atashikwa na hofu. Kisha atarudi nyuma huku amejaa hasira na atalitangua agano takatifu. Hapo atafuata shauri la wale walioasi agano takatifu. Wanajeshi wake watalitia najisi hekalu na ngome zake, watakomesha tambiko za kuteketezwa kila siku na kusimamisha huko hekaluni chukizo haribifu. Atawashawishi kwa hila wale walioasi agano, lakini watu walio waaminifu kwa Mungu wao watasimama imara na kuchukua hatua. Wenye hekima miongoni mwa watu watawafundisha wengi. Hata hivyo, kwa siku kadhaa watauawa kwa upanga au moto, watachukuliwa mateka au kunyanganywa mali zao. Wakati wanapouawa, watapata msaada kidogo, na wengi wanaojiunga nao, watafanya hivyo kwa unafiki. Baadhi ya wenye hekima watauawa, ili wapate kuondolewa uchafu, kutakaswa na kusafishwa, mpaka wakati wa mwisho, ambao sasa bado haujatimia. “ ‘Mfalme atafanya kama apendavyo. Atajitukuza na kujikweza kwamba yeye ni mkuu kuliko miungu yote, na kumkufuru Mungu wa miungu. Ataendelea kufanikiwa mpaka ghadhabu ifikie kikomo chake, kwani yaliyopangwa lazima yatimie. Mfalme huyo hataijali miungu ya wazee wake wala yule anayependwa na wanawake. Ataidharau miungu mingine yote, kwani atajiweka kuwa mkuu kuliko kila mmoja wao. Badala ya miungu hiyo atamheshimu mungu mlinzi wa ngome, ambaye wazee wake kamwe hawakumwabudu, atamtolea dhahabu, fedha na vito vya thamani, na zawadi za thamana kubwa. Atazishughulikia ngome zake kwa msaada wa mungu wa kigeni. Wale wanaomtambua kuwa mfalme, atawatunukia heshima kubwa, atawapa vyeo vikubwa na kuwagawia ardhi kama zawadi. “ ‘Wakati wa mwisho mfalme wa kusini atamshambulia mfalme huyo wa kaskazini. Lakini mfalme wa kaskazini atajibu mashambulio hayo kwa nguvu kama kimbunga, akitumia magari ya farasi, wapandafarasi na meli nyingi. Atazivamia nchi nyingi na kupita katika nchi hizo kama mafuriko ya maji. Ataivamia hata nchi ile tukufu na kuua maelfu ya watu. Lakini nchi za Edomu, Moabu na sehemu kubwa ya Amoni, zitaokoka kutoka mikononi mwake. Wakati atakapozivamia nchi hizo, hata nchi ya Misri haitanusurika. Atamiliki hazina za dhahabu, fedha na vito vyote vya thamani vya nchi ya Misri. Watu wa Libia na watu wa Kushi watafuata nyayo zake. Lakini habari kutoka mashariki na kaskazini zitamtisha. Naye atatoka kwa hasira kubwa ili kukatilia mbali na kuangamiza wengi. Zaidi ya hayo, atapiga mahema yake makubwa kati ya bahari na mlima mtukufu na mtakatifu. Lakini atakuwa amefikia kikomo chake, na hatakuwapo yeyote wa kumsaidia. “ ‘Wakati huo, Mikaeli, malaika mkuu, aliye mlinzi wa watu wako, atatokea. Ndipo kutakuwa na wakati wa taabu sana kuliko nyakati nyingine zote tangu mataifa yalipoanza kuwako duniani. Lakini, wakati huo, kila mmoja wa watu wako ambaye jina lake limeandikwa katika kitabu cha uhai, ataokolewa. Wengi wa wale ambao wamekwisha kufa, watafufuka; wengine watapata uhai wa milele, na wengine watapata uhai na kudharauliwa milele. Wale wenye hekima watangaa kama anga angavu, na wale waliowaongoza wengine kutenda mema, watangaa kama nyota milele. Ila sasa, Danieli, weka siri mambo hayo; kifunge kitabu na kukitia mhuri mpaka wakati wa mwisho utakapofika. Wengi watakimbilia huko na huko, na maarifa yataongezeka.’” “Kisha, mimi Danieli nikatazama, nikaona watu wawili wamesimama penye kingo za mto; mmoja upande huu na mwingine upande wa pili. Nikamwuliza yule aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, mambo haya ya kutisha yatadumu mpaka lini ndipo yaishe? Yule mtu aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, akainua mikono yake yote miwili kuelekea mbinguni. Kisha nikamsikia akiapa kwa jina la yule aishiye milele: ‘Itakuwa muda wa nyakati tatu na nusu. Wakati mateso ya watu watakatifu yatakapokomeshwa, mambo haya yote yatakuwa yametimia.’ Nilisikia lakini sikuelewa. Ndipo, nikamwuliza, ‘Bwana wangu, mwisho wa mambo haya yote utakuwaje?’ Akanijibu, ‘Danieli, sasa nenda zako, kwani maneno haya ni siri na yamefungwa kwa kutiwa mhuri mpaka wakati wa mwisho. Watu wengi wataondolewa uchafu, watatakaswa na kusafishwa. Lakini watu waovu wataendelea kutenda uovu. Hakuna hata mmoja wa hao waovu atakayeelewa; wenye hekima ndio watakaoelewa. “ ‘Tangu wakati wa kukomeshwa kwa sadaka za kuteketezwa kila siku, yaani kutoka wakati ule chukizo haribifu litakaposimamishwa itakuwa muda wa siku 1,290. Heri yao watakaostahimili mpaka siku zile 1,335 zitakapotimia. “ ‘Lakini wewe, ee Danieli, jiendee, ukapumzike kaburini, na wakati huo utakapotimia, utafufuka na kupata tuzo lako.’” Neno la Bwana lililomjia Hosea mwana wa Beeri, nyakati za Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli. Mwenyezi-Mungu alipoanza kuongea na Waisraeli kwa njia ya Hosea, alimwambia hivi: “Nenda ukaoe mwanamke mzinzi, uzae naye watoto wa uzinzi, maana watu wa nchi hii wanafanya uzinzi mwingi kwa kuniacha mimi.” Basi, Hosea akaenda, akamwoa Gomeri, binti Diblaimu. Gomeri akapata mimba, akamzalia Hosea mtoto wa kiume. Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Yezreeli’, maana bado kitambo kidogo tu, nami nitaiadhibu jamaa ya Yehu kwa mauaji aliyoyafanya bondeni Yezreeli. Nitaufutilia mbali ufalme katika taifa la Israeli. Siku hiyo, nitazivunja nguvu za kijeshi za Israeli huko bondeni Yezreeli.” Gomeri alipata mimba tena, akazaa mtoto wa kike. Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Asiyehurumiwa’, maana sitawahurumia tena Waisraeli wala sitawasamehe. Lakini nitawahurumia watu wa Yuda na kuwaokoa. Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, nitawaokoa, lakini si kwa nguvu za kijeshi, au pinde, au panga, au farasi au wapandafarasi.” Gomeri alipomwachisha kunyonya “Asiyehurumiwa,” alipata mimba tena, akamzalia Hosea mtoto mwingine wa kiume. Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Siwangu,’ maana nyinyi si watu wangu, wala mimi si wenu.” Lakini idadi ya Waisraeli itakuwa kubwa kama mchanga wa pwani ambao haupimiki wala hauhesabiki. Pale ambapo Mungu aliwaambia, “Nyinyi si watu wangu,” sasa atawaambia, “Nyinyi ni watoto wa Mungu aliye hai.” Watu wa Yuda na wa Israeli wataungana pamoja na kumchagua kiongozi wao mmoja; nao watastawi katika nchi yao. Hiyo itakuwa siku maarufu ya Yezreeli. Basi, waiteni kaka zenu, “Watu wangu,” na dada zenu, “Waliohurumiwa.” Mlaumuni mama yenu mlaumuni, maana sasa yeye si mke wangu wala mimi si mume wake. Mlaumuni aondokane na uasherati wake, ajiepushe na uzinzi wake. La sivyo, nitamvua nguo abaki uchi, nitamfanya awe kama alivyozaliwa. Nitamfanya awe kama jangwa, nitamweka akauke kama nchi kavu. Nitamuua kwa kiu. Na watoto wake sitawahurumia, maana ni watoto wa uzinzi. Mama yao amefanya uzinzi, aliyewachukua mimba amefanya mambo ya aibu. Alisema; “Nitaambatana na wapenzi wangu, ambao hunipa chakula na maji, sufu na kitani, mafuta na divai.” Basi, nitaiziba njia yake kwa miiba, nitamzungushia ukuta, asipate njia ya kutokea nje. Atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; naam, atawatafuta, lakini hatawaona. Hapo ndipo atakaposema, “Nitarudi kwa mume wangu wa kwanza; maana hapo kwanza nilikuwa nafuu kuliko sasa.” Hakujua kwamba ni mimi niliyempa nafaka, divai na mafuta, niliyemjalia fedha na dhahabu kwa wingi, ambazo alimpelekea Baali. Kwa hiyo wakati wa mavuno nitaichukua nafaka yangu, nitaiondoa divai yangu wakati wake. Nitamnyang'anya nguo zangu za sufu na kitani, ambazo zilitumika kuufunika uchi wake. Nitamvua abaki uchi mbele ya wapenzi wake, wala hakuna mtu atakayeweza kunizuia. Nitazikomesha starehe zake zote, sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato, na sikukuu zote zilizoamriwa. Nitaiharibu mizabibu yake na mitini, anayosema ni malipo kutoka kwa wapenzi wake. Nitaifanya iwe misitu, nao wanyama wa porini wataila. Nitamlipiza sikukuu za Baali alizoadhimisha, muda alioutumia kuwafukizia ubani, akajipamba kwa pete zake na johari, na kuwaendea wapenzi wake, akanisahau mimi. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema. Kwa hiyo, nitamshawishi, nitampeleka jangwani na kusema naye kwa upole. Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu, bonde la Akori nitalifanya lango la tumaini. Atanifuata kwa hiari kama alipokuwa kijana, kama wakati alipotoka katika nchi ya Misri. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku hiyo, wewe utaniita ‘Mume wangu,’ na sio tena ‘Baali wangu.’ Maana, nitalifanya jina la Baali lisitamkike tena kinywani mwako. Nitafanya agano na wanyama wa porini, ndege wa angani pamoja na vyote vitambaavyo, wasikuumize. Nitatokomeza upinde, upanga na silaha za vita katika nchi, na kukufanya uishi kwa usalama. Nitakufanya mke wangu milele; uwe wangu kwa uaminifu na haki, kwa fadhili na huruma. Naam, nitakuposa kwa uaminifu, nawe utanijua mimi Mwenyezi-Mungu. “Siku hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema, nitaikubali haja ya mbingu ya kunyesha mvua, mbingu nazo zitaikubali haja ya ardhi. Ardhi itaikubali haja ya nafaka, divai na mafuta, navyo vitatosheleza mahitaji ya Yezreeli. Nitamwotesha Yezreeli katika nchi; nitamhurumia ‘Asiyehurumiwa’, na wale walioitwa ‘Siwangu’, nitawaambia, ‘Nyinyi ni watu wangu.’ Nao watasema, ‘Wewe ni Mungu wetu.’” Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Nenda tena ukampende mwanamke anayependwa na mwanamume mwingine na ambaye ni mzinzi. Mpende kama mimi Mwenyezi-Mungu ninavyowapenda Waisraeli, ingawa wao wanaigeukia miungu mingine na kuwa na uchu wa maandazi ya zabibu kavu.” Basi, nikamnunua huyo mwanamke kwa vipande kumi na vitano vya fedha na magunia mengi ya shayiri. Kisha nikamwambia, “Lazima uwe wangu kwa siku nyingi bila kufanya uzinzi au kuwa mke wa mtu mwingine; nami pia nitakuwa mwaminifu.” Hivyo ndivyo Waisraeli watakavyokuwa: Watakaa kwa muda mrefu bila mfalme au mkuu; bila tambiko, wala mnara wala kizibao cha kifuani wala kinyago. Baadaye, Waisraeli watarudi na kumtafuta Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, na kumtafuta mfalme wao, mzawa wa Daudi. Ndipo watakapomcha Mwenyezi-Mungu, na kutazamia wema wake siku za mwisho. Msikilizeni Mwenyezi-Mungu, enyi Waisraeli. Mwenyezi-Mungu anawashutumu wakazi wa nchi hii. “Hamna tena uaminifu wala wema nchini; hamna anayemjua Mungu katika nchi hii. Kuapa, uongo, mauaji, wizi na uzinzi huzuka humo. Umwagaji damu hufuatana mfululizo. Kwa hiyo, nchi yote ni kame, wakazi wake wote wanaangamia pamoja na wanyama wa porini na ndege; hata samaki wa baharini wanaangamizwa. “Lakini watu wasilaumiwe, wasishutumiwe; maana mimi nakushutumu wewe kuhani. Wewe utajikwaa mchana, naye nabii atajikwaa pamoja nawe usiku. Nitamwangamiza mama yako Israeli. Watu wangu wameangamia kwa kutonijua, maana wewe kuhani umekataa mafundisho. Nimekukataa kuwa kuhani wangu. Kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, nami pia nitawasahau watoto wako. “Kadiri makuhani walivyoongezeka, ndivyo wote walivyozidi kuniasi. Basi, nitaigeuza fahari yao kuwa aibu. Wanajishibisha kwa sadaka za watu wangu wenye dhambi. Wana hamu sana ya kuwaona wametenda dhambi. Lakini yatakayowapata watu yatawapata makuhani; nitawaadhibu kwa sababu ya mwenendo wao, nitawalipiza matendo yao wenyewe. Watakula, lakini hawatashiba; watazini, lakini hawatapata watoto, kwa sababu wameniacha mimi Mwenyezi-Mungu, na kufuata miungu mingine. “Divai mpya na ya zamani huondoa maarifa. Watu wangu huomba shauri kutoka kwa mti; kijiti chao cha ramli ndicho kinachowapa kauli. Nia ya kufanya uzinzi imewapotosha; wamefanya uzinzi kwa kufuata miungu mingine, wakaniacha mimi Mungu wao. Wanatambikia kwenye vilele vya milima; naam, wanatoa tambiko vilimani, chini ya mialoni, migude na mikwaju, maana kivuli chao ni kizuri. “Kwa hiyo binti zenu hufanya uzinzi, na bibiarusi wenu hufanya uasherati. Lakini sitawaadhibu binti zenu wanapofanya uzinzi, wala bibi arusi wenu wanapofanya uasherati, maana, wanaume wenyewe ndio wanaofuatana na wazinzi, na kutambikia pamoja nao katika ibada za uzinzi. Watu hawa watovu wa akili hakika wataangamia! “Ama kweli nyinyi Waisraeli ni wazinzi! Lakini, msiwafanye watu wa Yuda wawe na hatia! Msiende mahali patakatifu huko Gilgali, wala msiende kule Beth-aveni. Wala msiape mkisema, ‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo!’” Waisraeli ni wakaidi kama punda. Kwa nini basi Mungu ashughulike kuwachunga, kama kondoo kwenye malisho mapana? “Watu wa Efraimu wamejifunga na sanamu. Haya! Waache waendelee tu! Kama vile genge la walevi, wanajitosa wenyewe katika uzinzi; wanapendelea aibu kuliko heshima yao. Basi, kimbunga kitawapeperusha, na watayaonea aibu matambiko yao kwa miungu ya uongo. “Haya! Sikilizeni enyi makuhani! Tegeni sikio, enyi Waisraeli! Sikilizeni enyi ukoo wa kifalme! Nyinyi mlipaswa kuzingatia haki, badala yake mmekuwa mtego huko Mizpa, mmekuwa wavu wa kuwanasa huko Tabori. Mmechimba shimo refu la kuwanasa huko Shitimu. Lakini mimi nitawaadhibuni nyote. Nawajua watu wa Efraimu, Waisraeli hawakufichika kwangu. Nyinyi watu wa Efraimu mmefanya uzinzi, watu wote wa Israeli wamejitia najisi. “Matendo yao yanawazuia wasimrudie Mungu wao. Mioyoni mwao wamejaa uzinzi; hawanijui mimi Mwenyezi-Mungu. Kiburi cha Waisraeli chaonekana wazi; watu wa Efraimu watajikwaa katika hatia yao, nao watu wa Yuda watajikwaa pamoja nao. Watakwenda na makundi yao ya kondoo na ng'ombe, kumtafuta Mwenyezi-Mungu; lakini hawataweza kumpata, kwa sababu amejitenga nao. Wamevunja uaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, wamezaa watoto walio haramu. Mwezi mwandamo utawaangamiza, pamoja na mashamba yao. “Pigeni baragumu huko Gibea, na tarumbeta huko Rama. Pigeni king'ora huko Beth-aveni. Enyi watu wa Benyamini, adui yenu yuko nyuma! Siku nitakapotoa adhabu Efraimu itakuwa kama jangwa! Ninachotangaza miongoni mwa makabila ya Israeli, ni jambo litakalotukia kwa hakika. Viongozi wa Yuda wamekuwa wenye kubadili mipaka ya ardhi. Mimi nitawamwagia hasira yangu kama maji. Efraimu ameteswa, haki zake zimetwaliwa; kwani alipania kufuata upuuzi. Hivyo mimi Mungu niko kama nondo kwa Efraimu, kama donda baya kwa watu wa Yuda. Watu wa Efraimu walipogundua ugonjwa wao, naam, watu wa Yuda walipogundua donda lao, watu wa Efraimu walikwenda Ashuru kuomba msaada kwa mfalme mkuu; lakini yeye hakuweza kuwatibu, hakuweza kuponya donda lenu. Maana mimi nitakuwa kama simba kwa Efraimu, kama mwanasimba kwa watu wa Yuda. Mimi mwenyewe nitawararua na kuondoka, nitawachukua na hakuna atakayewaokoa. Nitarudi mahali pangu na kujitenga nao mpaka wakiri kosa lao na kunirudia. Taabu zao zitawafundisha wanitafute, wakisema: “ ‘Twendeni, tukamrudie Mwenyezi-Mungu! Yeye mwenyewe ameturarua, lakini yeye mwenyewe atatuponya. Yeye mwenyewe ametujeruhi, lakini yeye mwenyewe atatibu majeraha yetu. Baada ya siku mbili, atatupa uhai tena, naam, siku ya tatu atatufufua ili tuweze kuishi pamoja naye. Basi tumtambue, tujitahidi kumjua Mwenyezi-Mungu. Kuja kwake ni hakika kama alfajiri, yeye atatujia kama manyunyu, kama mvua za masika ziinyweshayo ardhi.’” Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nitakutendea nini ee Efraimu? Nikufanyie nini ee Yuda? Upendo wenu kwangu ni kama ukungu wa asubuhi, kama umande unaotoweka upesi. Ndiyo maana nimewavamia kwa njia ya manabii, nimewaangamiza kwa maneno yangu, hukumu yangu huchomoza kama pambazuko. Maana ninachotaka kwenu ni upendo na si tambiko, Kumjua Mungu na si kutoa sadaka za kuteketezwa. “Lakini mlilivunja agano langu kama mlivyofanya mjini Adamu; huko walinikosea uaminifu. Gileadi ni mji wa waovu, umetapakaa damu. Kama wanyang'anyi wamwoteavyo mtu njiani, ndivyo na makuhani walivyojikusanya na kuvizia. Wanaua watu njiani kuelekea Shekemu, naam, wanatenda uovu kupindukia. Nimeona jambo la kuchukiza sana miongoni mwa Waisraeli: Watu wa Efraimu wanakimbilia miungu mingine naam, Waisraeli wamejitia unajisi. Nawe Yuda hali kadhalika, nimekupangia wakati utakapovuna adhabu. Kila nikitaka kuwarekebisha watu wangu, ninapotaka kuwaponya Waisraeli, uovu wa watu wa Efraimu hufunuliwa, matendo mabaya ya Samaria hujitokeza. Wao huongozwa na udanganyifu, kwenye nyumba wezi huvunja nje barabarani wanyang'anyi huvamia. Hawafikiri hata kidogo kwamba mimi nayakumbuka maovu yao yote. Sasa maovu yao yamewabana. Yote waliyotenda yako mbele yangu. “Wanamfurahisha mfalme kwa maovu yao wanawafurahisha wakuu kwa uhaini wao. Wote ni wazinzi; wao ni kama tanuri iliyowashwa moto ambao mwokaji hauchochei tangu akande unga mpaka mkate utakapoumuka. Kwenye sikukuu ya mfalme, waliwalewesha sana maofisa wake; naye mfalme akashirikiana na wahuni. Kama tanuri iwakavyo, mioyo yao huwaka kwa hila; usiku kucha hasira yao hufuka moshi, ifikapo asubuhi, hulipuka kama miali ya moto. Wote wamewaka hasira kama tanuri, na wanawaangamiza watawala wao. Wafalme wao wote wameanguka, wala hakuna anayeniomba msaada. “Efraimu amechanganyika na watu wa mataifa. Anaonekana kama mkate ambao haukugeuzwa. Wageni wamezinyonya nguvu zake, wala yeye mwenyewe hajui; mvi zimetapakaa kichwani mwake, lakini mwenyewe hana habari. Kiburi cha Waisraeli chashuhudia dhidi yao, hawanirudii mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao; wala hawanitafuti kwa matukio hayo yote. Efraimu ni kama njiwa, mjinga asiye na akili; mara yuko Misri, mara Ashuru kuomba. Watakapokwenda nitatandaza wavu wangu niwanase, nitawaangusha chini kama ndege wa angani; nitamwaadhibu kadiri ya ripoti ya maovu yao. Ole wao kwa kuwa wameniacha! Maangamizi na yawapate, maana wameniasi. Nilitaka kuwakomboa, lakini wanazua uongo dhidi yangu. “Wananililia, lakini si kwa moyo. Wanagaagaa na kujikatakata vitandani mwao, kusudi nisikilize dua zao za nafaka na divai; lakini wanabaki waasi dhidi yangu. Mimi ndimi niliyeiimarisha mikono yao, lakini wanafikiria maovu dhidi yangu. Wanaigeukia miungu batili, wako kama uta uliolegea. Viongozi wao watakufa kwa upanga, kwa sababu ya maneno yao ya kiburi. Kwa hiyo, watadharauliwa nchini Misri. “Pigeni baragumu! Adui anakuja kama tai kuivamia nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa wamelivunja agano langu na kuiasi sheria yangu. Waisraeli hunililia wakisema: ‘Mungu wetu, sisi tunakujua.’ Lakini Israeli amepuuza mambo mema, kwa hiyo, sasa adui watamfuatia. “Walijiwekea wafalme bila kibali changu, walijiteulia viongozi ambao sikuwatambua. Wamejitengenezea miungu ya fedha na dhahabu, jambo ambalo litawaangamiza. Watu wa Samaria, naichukia sanamu yenu ya ndama. Hasira yangu inawaka dhidi yenu. Mtaendelea mpaka lini kuwa na hatia? Nanyi Waisraeli ni hivyohivyo! Na sanamu yenu hiyo fundi ndiye aliyeitengeneza. Yenyewe si Mungu hata kidogo. Naam! Sanamu ya ndama ya Samaria itavunjwavunjwa! “Wanapanda upepo, watavuna kimbunga! Mimea yao ya nafaka iliyo mashambani haitatoa nafaka yoyote. Na hata kama ikizaa, mazao yake yataliwa na wageni. Waisraeli wamemezwa; sasa wamo kati ya mataifa mengine, kama chombo kisicho na faida yoyote; kwa kuwa wamekwenda kuomba msaada Ashuru. Efraimu ni punda anayetangatanga peke yake; Efraimu amekodisha wapenzi wake. Wametafuta wapenzi kati ya watu wa mataifa, lakini mimi nitawakusanya mara. Na hapo watasikia uzito wa mzigo, ambao mfalme wa wakuu aliwatwika. “Watu wa Efraimu wamejijengea madhabahu nyingi, na madhabahu hizo zimewazidishia dhambi. Hata kama ningewaandikia sheria zangu mara nyingi, wao wangeziona kuwa kitu cha kigeni tu. Wanapenda kutoa tambiko, na kula nyama yake; lakini mimi Mwenyezi-Mungu sipendezwi hata kidogo. Mimi nayakumbuka makosa yao; nitawaadhibu kwa dhambi zao; nitawarudisha utumwani Misri. Waisraeli wamemsahau Muumba wao, wakajijengea majumba ya fahari; watu wa Yuda wamejiongezea miji ya ngome, lakini mimi nitaipelekea moto miji hiyo, na kuziteketeza ngome zao.” Msifurahi enyi Waisraeli! Msifanye sherehe kama mataifa mengine; maana, mmekuwa wazinzi kwa kumwacha Mungu wenu. Mmefurahia malipo ya uzinzi, kila mahali pa kupuria nafaka. Lakini ngano na mapipa ya divai haitawalisha, hamtapata divai mpya. Hawatakaa katika nchi ya Mwenyezi-Mungu; naam, watu wa Efraimu watarudi utumwani Misri; watakula vyakula najisi huko Ashuru. Hawatamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya divai, wala hawatamfurahisha kwa tambiko zao. Chakula chao kitakuwa kama cha matanga, wote watakaokila watatiwa unajisi. Kitakuwa chakula cha kuwashibisha tu, hakitafaa kuletwa nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu. Mtafanya nini katika sikukuu ile iliyopangwa, au katika karamu ya Mwenyezi-Mungu? Mtakapoyakimbia maangamizi ya nchi yenu, Misri itawakaribisheni kwake, lakini makaburi yenu yawangoja huko Memfisi. Magugu yatamiliki hazina zenu za fedha, miiba itajaa katika mahema yenu. Siku za adhabu zimewadia, naam, siku za kulipiza kisasi zimefika; Waisraeli lazima wautambue wakati huo! Nyinyi mnasema, “Nabii ni mpumbavu; anayeongozwa na roho ni mwendawazimu.” Mnasema hivyo kwa sababu ya uovu wenu mkubwa, kwa sababu ya chuki yenu kali dhidi yake. Nabii ni mlinzi wa Waefraimu kwa niaba ya Mungu; lakini, kokote aendako anategewa mtego kama ndege. Hata nyumbani mwa Mungu wake anachukiwa. Nyinyi mmezama katika uovu, kama ilivyokuwa kule Gibea. Mungu atayakumbuka makosa yao, na kuwaadhibu kwa dhambi zao. Mwenyezi-Mungu asema: “Nilipowakuta Waisraeli walikuwa kama zabibu jangwani. Nilipowaona wazee wenu walikuwa bora kama tini za kwanza. Lakini mara walipofika huko Baal-peori, walijiweka wakfu kuabudu chukizo Baali, wakawa chukizo kama hicho walichokipenda. Fahari ya Efraimu itatoweka kama ndege; watoto hawatazaliwa tena, hakutakuwa na watoto wa kuzaliwa, wala hakutakuwa na kuchukuliwa mimba! Hata kama wakilea watoto, sitamwacha hai hata mmoja wao. Ole wao, nitakapowaacha peke yao!” Kama nilivyokwisha ona hapo kwanza, Efraimu alikuwa kama mtende mchanga penye konde zuri; lakini sasa Efraimu itamlazimu kuwapeleka watoto wake wauawe. Uwaadhibu watu hawa ee Mwenyezi-Mungu! Lakini utawaadhibu namna gani? Uwafanye wanawake wao kuwa tasa; uwafanye wakose maziwa ya kunyonyesha watoto wao! Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Uovu wao wote ulianzia Gilgali; huko ndiko nilipoanza kuwachukia. Kwa sababu ya uovu wa matendo yao, nitawafukuza nyumbani kwangu. Sitawapenda tena. Viongozi wao wote ni waasi. Watu wa Efraimu wamepigwa, wamekuwa kama mti wenye mzizi mkavu, hawatazaa watoto wowote. Hata kama wakizaa watoto, nitawaua watoto wao wawapendao.” Kwa vile wamekataa kumsikiliza, Mungu wangu atawatupa; wao watatangatanga kati ya mataifa. Waisraeli walikuwa kama mzabibu mzuri, mzabibu wenye kuzaa matunda. Kadiri matunda yalivyozidi kuongezeka, ndivyo walivyozidi kujijengea madhabahu. Kadiri nchi yao ilivyozidi kustawi, ndivyo walivyozidi kupamba nguzo zao za ibada. Mioyo yao imejaa udanganyifu. Sasa ni lazima wawajibike kwa hatia yao. Mwenyezi-Mungu atazibomoa madhabahu zao na kuziharibu nguzo zao. Wakati huo watasema: “Hatuna tena mfalme, kwa kuwa hatumchi Mwenyezi-Mungu; lakini, naye mfalme atatufanyia nini?” Wanachosema ni maneno matupu; wanaapa na kufanya mikataba ya bure; haki imekuwa si haki tena, inachipua kama magugu ya sumu shambani. Wakazi wa Samaria watatetemeka kwa sababu ya ndama wa huko Betheli. Watu wake watamwombolezea ndama huyo, hata makuhani wanaomwabudu watamlilia; kwani fahari ya ndama huyo imeondolewa. Kinyago hicho kitapelekwa Ashuru, kama ushuru kwa mfalme mkuu. Watu wa Efraimu wataaibishwa, Waisraeli watakionea aibu kinyago chao. Mfalme wa Samaria atachukuliwa, kama kipande cha mti juu ya maji. Mahali pa kuabudia vilimani pa Aweni, dhambi ya Waisraeli, pataharibiwa. Miiba na magugu vitamea katika madhabahu zao. Nao wataiambia milima, “Tufunikeni” na vilima, “Tuangukieni!” Enyi Waisraeli, nyinyi mmetenda dhambi tangu kule Gibea, na bado mnaendelea. Hakika vita vitawaangamiza hukohuko Gibea. Nitawajia watu hawa wapotovu na kuwaadhibu; watu wa mataifa watakusanyika kuwashambulia, watakapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao nyingi. Efraimu ni ndama aliyefundishwa vizuri, akapenda kupura nafaka. Lakini sasa shingo yake nzuri nitaifunga nira. Yuda atalima kwa jembe yeye mwenyewe, naam, Yakobo atakokota jembe la kupalilia. Pandeni wema kwa faida yenu, nanyi mtavuna upendo; limeni mashamba yaliyoachwa, maana wakati wa kunitafuta mimi Bwana umefika nami nitawanyeshea baraka. Lakini nyinyi mmepanda uovu, nyinyi mmevuna dhuluma; mmekula matunda ya uongo wenu. Wewe Israeli ulitegemea nguvu zako mwenyewe, na wingi wa askari wako. Kwa hiyo msukosuko wa vita utawajia watu wako; ngome zako zote zitaharibiwa, kama Shalmani alivyoharibu Beth-arbeli vitani, kina mama wakapondwa pamoja na watoto wao. Ndivyo itakavyokuwa kwenu enyi watu wa Betheli, kwa sababu ya uovu wenu mkuu. Kutakapopambazuka mfalme wa Israeli atawatokomeza. “Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda, Kutoka Misri nilimwita mwanangu. Lakini kadiri nilivyozidi kuwaita, ndivyo walivyozidi kwenda mbali nami; waliendelea kuyatambikia Mabaali, na kuvifukizia ubani vinyago vya miungu. Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea! Mimi mwenyewe niliwachukua mikononi mwangu; lakini hawakutambua kuwa mimi ndiye niliyewatunza. Niliwaongoza kwa kamba za huruma naam, kwa kamba za upendo; kama baba amwinuaye mtoto mpaka shavuni mwake, ndivyo nami nilivyokuwa kwao. Mimi niliinama chini na kuwalisha. Basi, watarudi nchini Misri; watatawaliwa na mfalme wa Ashuru, kwa sababu wamekataa kunirudia. “Upanga utavuma katika miji yao, utavunjavunja miimo ya malango yake na kuwaangamiza katika ngome zao. Watu wangu wamepania kuniacha mimi, wakiitwa waje juu, hakuna hata mmoja anayeweza. Ewe Efraimu, nawezaje kukuacha? Nawezaje kukutupa ewe Israeli? Nitawezaje kukufanya kama mji wa Adma? Nitawezaje kukutenda kama Seboimu! Nazuiwa na moyo wangu; huruma yangu imezidi kuwa motomoto. Nitaizuia hasira yangu kali; sitamwangamiza tena Efraimu, maana mimi ni Mungu, wala si binadamu. “Mimi ndimi Mtakatifu miongoni mwenu, nami sitakuja kuwaangamiza. “Watanifuata mimi Mwenyezi-Mungu ningurumaye kama simba; nitakaponguruma watanijia toka magharibi wakitetemeka. Watakuja kutoka Misri wakitetemeka kama ndege, wataruka kutoka Ashuru kama hua nami nitawarudisha makwao; mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Watu wa Efraimu wananirundikia uongo, na Waisraeli udanganyifu. Watu wa Yuda, wananiasi mimi Mungu Mtakatifu. Watu wa Efraimu wananirundikia uongo, na Waisraeli udanganyifu. Watu wa Yuda, wananiasi mimi Mungu Mtakatifu. “Watu wa Efraimu wanachunga upepo kutwa nzima wanafukuza upepo wa mashariki. Wanazidisha uongo na ukatili, wanafanya mkataba na Ashuru na kupeleka mafuta Misri.” Mwenyezi-Mungu ana mashtaka dhidi ya Yuda; atawaadhibu wazawa wa Yakobo kadiri ya makosa yao, na kuwalipa kadiri ya matendo yao. Yakobo akiwa bado tumboni mwa mama yake, alimshika kisigino kaka yake. Na alipokuwa mtu mzima alishindana na Mungu. Alipambana na malaika, akamshinda; alilia machozi na kuomba ahurumiwe. Huko Betheli, alikutana na Mungu, huko Mungu aliongea naye. Mwenyezi-Mungu, wa majeshi, Mwenyezi-Mungu, ndilo jina lake. Lakini nyinyi mrudieni Mungu wenu. Zingatieni upendo na haki, mtumainieni Mungu wenu daima. “Efraimu ni sawa na mfanyabiashara atumiaye mizani danganyifu, apendaye kudhulumu watu. Efraimu amesema, ‘Mimi ni tajiri! Mimi nimejitajirisha! Hamna ubaya kupata faida. Hata hivyo, hilo si kosa!’” Mwenyezi-Mungu asema, “Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; mimi ndimi niliyekutoa nchini Misri! Mimi nitakukalisha tena katika mahema, kama ufanyavyo sasa kwa siku chache tu, wakati wa sikukuu ya vibanda. Mimi niliongea na manabii; ni mimi niliyewapa maono mengi, na kwa njia yao natangaza mpango wangu. Huko Gileadi ni mahali pa dhambi; huko Gilgali walitambika fahali, kwa hiyo madhabahu zao zitakuwa marundo ya mawe kwenye mitaro shambani.” Yakobo alikimbia nchi ya Aramu akiwa huko alifanya kazi apate mke, akachunga kondoo ili apate mke. Kwa nabii Mwenyezi-Mungu aliwatoa Waisraeli nchini Misri, na kwa nabii Mungu aliwahifadhi. Waefraimu wamemchukiza Mwenyezi-Mungu sana. Lakini Mwenyezi-Mungu atawalipiza makosa yao, atawaadhibu kwa mambo maovu waliyotenda. Waefraimu waliponena, watu walitetemeka; Waefraimu walikuwa na uwezo mkubwa huko Israeli, lakini walianza kumwabudu Baali, wakajiletea kifo. Waefraimu wameendelea kutenda dhambi, wakajitengenezea sanamu za kusubu, sanamu zilizotengenezwa kwa ustadi wao, zote zikiwa kazi ya mafundi. Wanasema, “Haya zitambikieni!” Wanaume wanabusu ndama! Basi, watatoweka kama ukungu wa asubuhi, kama umande utowekao upesi; kama makapi yanayopeperushwa mahali pa kupuria, kama moshi unaotoka katika bomba. Mwenyezi-Mungu asema: “Lakini mimi, Mwenyezi-Mungu, ni Mungu wenu, ambaye niliwatoa nchini Misri; hamna mungu mwingine ila mimi, wala hakuna awezaye kuwaokoeni. Ni mimi niliyewatunza mlipokuwa jangwani, katika nchi iliyokuwa ya ukame. Lakini mlipokwisha kula na kushiba, mlianza kuwa na kiburi, mpaka mkanisahau. Basi, nitakuwa kama simba kwenu nyote; nitawavizieni kama chui njiani. Nitawarukieni kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake. Nitawararua vifua vyenu na kuwala papo hapo kama simba; nitawararua vipandevipande kama mnyama wa porini. “Nitawaangamiza, enyi Waisraeli. Nani ataweza kuwasaidia? Yuko wapi sasa mfalme wenu awaokoe? Wako wapi wale wakuu wenu wawalinde? Nyinyi ndio mlioomba: ‘Tupatie mfalme na wakuu watutawale.’ Kwa hasira yangu mimi nikawapa mfalme, kisha nikamwondoa kwa ghadhabu yangu. “Uovu wa Efraimu uko umeandikwa, dhambi yake imehifadhiwa ghalani. Maumivu kama ya kujifungua mtoto yanamfikia. Lakini yeye ni mtoto mpumbavu; wakati ufikapo wa kuzaliwa yeye hukataa kutoka tumboni kwa mama! Yanibidi kuwakomboa hawa watu kutoka kuzimu; sharti niwaokoe kutoka kifoni! Ewe Kifo, yako wapi maafa yako? Ewe Kuzimu, yako wapi maangamizi yako? Mimi sitawaonea tena huruma! “Hata kama Efraimu atastawi kama nyasi, mimi Mwenyezi-Mungu nitavumisha upepo wa mashariki, upepo utakaozuka huko jangwani, navyo visima vyake vitakwisha maji, chemchemi zake zitakauka. Hazina zake zote za thamani zitanyakuliwa.” Watu wa Samaria wataadhibiwa kwa kosa lao. Kwa sababu wamemwasi Mungu wao. Watauawa kwa upanga, vitoto vyao vitapondwapondwa, na kina mama wajawazito watatumbuliwa. Enyi Waisraeli, mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mmejikwaa kwa sababu ya uovu wenu. Ombeni toba kwake, mrudieni na kumwambia: “Utusamehe uovu wote, upokee zawadi zetu, nasi tutakusifu kwa moyo. Ashuru haitatuokoa, hatutategemea tena farasi wa vita. Hatutaviita tena: ‘Mungu wetu’ hivyo vinyago tulivyochonga wenyewe. Kwako ee Mungu yatima hupata huruma.” Mwenyezi-Mungu asema, “Nitaponya utovu wao wa uaminifu; nitawapenda tena kwa hiari yangu, maana sitawakasirikia tena. Nitakuwa kama umande kwa Waisraeli nao watachanua kama yungiyungi, watakuwa na mizizi kama mwerezi wa Lebanoni. Chipukizi zao zitatanda na kuenea, uzuri wao utakuwa kama mizeituni, harufu yao nzuri kama maua ya Lebanoni. Watarudi na kuishi chini ya ulinzi wangu, watastawi kama bustani nzuri. Watachanua kama mzabibu, harufu yao nzuri kama ya divai ya Lebanoni. Enyi watu wa Efraimu, mna haja gani tena na sanamu? Mimi ndiye ninayesikiliza sala zenu, mimi ndiye ninayewatunzeni. Mimi nitawapa kivuli kama mberoshi, kutoka kwangu mtapata matunda yenu. Yeyote aliye na hekima ayaelewe mambo haya, mtu aliye na busara ayatambue. Maana njia za Mwenyezi-Mungu ni nyofu; watu wanyofu huzifuata, lakini wakosefu hujikwaa humo.” Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli: Sikilizeni kitu hiki enyi wazee; tegeni sikio wakazi wote wa Yuda! Je, jambo kama hili limewahi kutokea maishani mwenu, au nyakati za wazee wenu? Wasimulieni watoto wenu jambo hili, nao wawasimulie watoto wao, na watoto wao wakisimulie kizazi kifuatacho. Nzige, makundi kwa makundi, wameivamia mimea; kilichoachwa na nzige kimeliwa na tunutu, kilichoachwa na tunutu kimeliwa na parare, kilichoachwa na parare kimeliwa na matumatu. Enyi walevi, levukeni na kulia; pigeni yowe, enyi walevi wa divai; zabibu zote za kutengeneza divai mpya zimeharibiwa. Jeshi la nzige limeivamia nchi yetu; lina nguvu na ni kubwa ajabu; meno yake ni kama ya simba, na magego yake ni kama ya simba jike. Limeiharibu mizabibu yetu, na kuitafuna mitini yetu. Limeyabambua magamba yake na kuyatupa chini, na matawi yake yameachwa meupe. Lieni kama msichana aliyevaa vazi la gunia akiombolezea kifo cha mchumba wake. Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu. Makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu, wanaomboleza. Mashamba yamebaki matupu; nchi inaomboleza, maana nafaka imeharibiwa, divai imetoweka, mafuta yamekosekana. Ombolezeni enyi wakulima; pigeni yowe enyi watunza mizabibu. Ngano na shayiri zimeharibika, mavuno yote shambani yameangamia. Mizabibu imenyauka; mitini imedhoofika; mikomamanga, mitende na mitofaa imekauka, naam miti yote shambani imekauka. Furaha imetoweka miongoni mwa watu. Enyi makuhani, jivikeni magunia kuomboleza, lieni enyi wahudumu wa madhabahu. Ingieni hekaluni mkaomboleze usiku kucha! Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mungu. Toeni amri watu wafunge; itisheni mkutano wa kidini. Kusanyeni wazee na wakazi wote wa nchi, nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na humo mkamlilie Mwenyezi-Mungu. Ole wetu kwa ile siku ya Mwenyezi-Mungu, siku hiyo ya Mwenyezi-Mungu inakaribia; inakuja pamoja na maangamizi, kutoka kwa Mungu Mkuu. Mazao yetu yameharibiwa huku tunatazama. Furaha na kicheko vimetoweka nyumbani kwa Mungu wetu. Mbegu zinaoza udongoni; ghala za nafaka ni ukiwa mtupu, ghala zimeharibika, kwa kukosa nafaka ya kuhifadhi. Tazama wanyama wanavyolia kwa huzuni! Makundi ya ng'ombe yanahangaika, kwa sababu yamekosa malisho; hata makundi ya kondoo yanateseka. Ninakulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu, moto umemaliza malisho nyikani, miali ya moto imeteketeza miti mashambani. Hata wanyama wa porini wanakulilia wewe, maana, vijito vya maji vimekauka, moto umemaliza malisho nyikani. Pigeni tarumbeta huko Siyoni; pigeni baragumu juu ya mlima mtakatifu! Tetemekeni enyi wakazi wa Yuda, maana siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja, naam, siku hiyo iko karibu! Hiyo ni siku ya giza na huzuni; siku ya mawingu na giza nene. Jeshi kubwa la nzige linakaribia kama giza linalotanda milimani. Namna hiyo haijapata kuweko kamwe wala haitaonekana tena katika vizazi vyote vijavyo. Kama vile moto uteketezavyo jeshi hilo laharibu kila kitu mbele yake na kuacha nyuma kila kitu kinateketezwa; kabla hawajapita, nchi ni kama bustani ya Edeni, lakini wakisha pita, ni jangwa tupu. Hakuna kiwezacho kuwaepa! Wanaonekana kama farasi, wanashambulia kama farasi wa vita, Wanaporukaruka kwenye vilele vya milima, wanarindima kama magari ya farasi, wanavuma kama mabua makavu motoni. Wamejipanga kama jeshi kubwa tayari kabisa kufanya vita. Wakaribiapo, watu hujaa hofu, nyuso zao zinawaiva. Wanashambulia kama mashujaa wa vita; kuta wanazipanda kama wanajeshi. Wote wanakwenda mbele moja kwa moja, bila hata mmoja wao kubadilisha njia. Hakuna amsukumaye mwenziwe; kila mmoja anafuata mkondo wake. Wanapita kati ya vizuizi vya silaha, wala hakuna kiwezacho kuwazuia. Wanauvamia mji, wanapiga mbio ukutani; wanaziparamia nyumba na kuingia, wanapenya madirishani kama wezi. Nchi inatetemeka mbele yao, mbingu zinatikisika. Jua na mwezi vyatiwa giza, nazo nyota zinaacha kuangaza. Mwenyezi-Mungu anaamuru jeshi lake kwa sauti; askari wake ni wengi mno, wanaomtii hawahesabiki. 2Siku ya Mwenyezi-Mungu kweli ni kuu na ya kutisha sana! Nani atakayeweza kuistahimili? “Lakini hata sasa,” nasema mimi Mwenyezi-Mungu, “Nirudieni kwa moyo wote, kwa kufunga, kulia na kuomboleza. Msirarue mavazi yenu kuonesha huzuni bali nirudieni kwa moyo wa toba.” Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; yeye amejaa neema na huruma; hakasiriki upesi, ni mwingi wa fadhili; daima yu tayari kuacha kuadhibu. Huenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atabadili nia na kuwapeni baraka ya mazao, mkamtolea sadaka za nafaka na kinywaji. Pigeni tarumbeta huko Siyoni! Toeni amri watu wafunge; itisheni mkutano wa kidini. Wakusanyeni watu wote, wawekeni watu wakfu. Waleteni wazee, wakusanyeni watoto, hata watoto wanyonyao. Bwana arusi na bibi arusi na watoke vyumbani mwao. Kati ya madhabahu na lango la hekalu, makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu, walie na kuomba wakisema: “Wahurumie watu wako, ee Mwenyezi-Mungu. Usiyaache mataifa mengine yatudharau na kutudhihaki yakisema, ‘Yuko wapi basi Mungu wao?’” Ndipo Mwenyezi-Mungu akaipenda nchi yake akawahurumia watu wake. Alisikiliza, akajibu sala zao; akasema, “Sasa nitawapeni tena nafaka, sitawafanya mdharauliwe tena na mataifa. Nitawaondoa hao adui watokao kaskazini, nitawafukuza mpaka jangwani; askari wa mbele nitawatupa katika Bahari ya Chumvi na wale wa nyuma katika Bahari ya Mediteranea. Watatoa uvundo na harufu mbaya, hao ambao wamefanya maovu makubwa. “Usiogope, ewe nchi, bali furahi na kushangilia, maana Mwenyezi-Mungu ametenda makuu. Msiogope, enyi wanyama. malisho ya nyikani yamekuwa mazuri, miti inazaa matunda yake, mizabibu na mitini zinazaa kwa wingi. “Furahini, enyi watu wa Siyoni, shangilieni kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, maana amewapeni mvua za masika, amewapeni mvua ya kutosha: Mvua za masika na mvua za vuli kama hapo awali. Mahali pa kupuria patajaa nafaka, mashinikizo yatafurika divai na mafuta. Nitawarudishia miaka ile iliyoliwa na nzige, kila kitu kilicholiwa na tunutu, parare na matumatu, hilo jeshi kubwa nililowaletea! Mtapata chakula kingi na kutosheka; mtalisifu jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu. Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena. Mtatambua kwamba mimi nimo miongoni mwenu, enyi Waisraeli; kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, ndimi Mungu wenu wala hakuna mwingine. Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena. “Kisha hapo baadaye nitaimimina roho yangu juu ya binadamu wote. Watoto wenu wa kike na wa kiume watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono. Hata juu ya watumishi wa kiume na wa kike, nitaimimina roho yangu wakati huo. “Nitatoa ishara mbinguni na duniani; kutakuwa na damu, moto na minara ya moshi. Jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kufika siku ya Mwenyezi-Mungu, siku iliyo kuu na ya kutisha. Hapo watu wote watakaoomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu wataokolewa. Maana katika mlima Siyoni na Yerusalemu, watakuwako watu watakaosalimika, kama nilivyosema mimi Mwenyezi-Mungu. “Wakati huo na siku hizo nitakapoirekebisha hali ya Yuda na Yerusalemu, nitayakusanya mataifa yote, niyapeleke katika bonde liitwalo, ‘Mwenyezi-Mungu Ahukumu. Huko nitayahukumu mataifa hayo, kwa mambo yaliyowatendea watu wangu Israeli, hao walio mali yangu mimi mwenyewe. Maana waliwatawanya miongoni mwa mataifa, waligawa nchi yangu na kugawana watu wangu kwa kura. Waliwauza wavulana ili kulipia malaya, na wasichana ili kulipia divai. “Mnataka kunifanya nini enyi Tiro na Sidoni na maeneo yote ya Filistia? Je, mna kisasi nami mnachotaka kulipiza? Kama mnalipiza kisasi, mimi nitawalipizeni mara moja! Mmechukua fedha na dhahabu yangu, na kuvibeba vitu vyangu vya thamani hadi kwenye mahekalu yenu. Mmewapeleka watu wa Yuda na Yerusalemu mbali na nchi yao, mkawauza kwa Wagiriki. Sasa, nitawarudisha watu wangu kutoka huko mlikowauza. Nitawalipizeni kisasi kwa yote mliyowatendea. Watoto wenu wa kiume na wa kike nitawafanya wauzwe kwa watu wa Yuda, nao watawauzia Washeba, watu wa taifa la mbali kabisa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Watangazieni watu wa mataifa jambo hili: Jitayarisheni kwa vita, waiteni mashujaa wenu; askari wote na wakusanyike, waende mbele. Majembe yenu yafueni yawe mapanga, miundu yenu ya kupogolea iwe mikuki. Hata aliye dhaifu na aseme: ‘Mimi pia ni shujaa’. Njoni haraka, enyi mataifa yote jirani, kusanyikeni huko bondeni.” Ee Mwenyezi-Mungu! Teremsha askari wako dhidi yao! “Haya mataifa na yajiweke tayari; yaje kwenye bonde liitwalo: ‘Mwenyezi-Mungu Ahukumu’. Huko, mimi Mwenyezi-Mungu, nitaketi kuyahukumu mataifa yote ya jirani. Haya! Chukueni mundu wa kuvuna, kwani sasa ni wakati wa mavuno. Ingieni! Wapondeni kama zabibu ambazo zimejaza shinikizo. Uovu wao umepita kiasi kama mapipa yanayofurika.” Wanafika makundi kwa makundi kwenye bonde la Hukumu, maana siku ya Mwenyezi-Mungu imekaribia. Jua na mwezi vinatiwa giza, na nyota zimeacha kuangaza. Mwenyezi-Mungu ananguruma huko Siyoni; sauti yake inavuma kutoka Yerusalemu; mbingu na dunia vinatetemeka. Lakini Mwenyezi-Mungu ni kimbilio la watu wake, ni ngome ya usalama kwa Waisraeli. “Hapo, ewe Israeli, utajua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nakaa Siyoni, mlima wangu mtakatifu, Yerusalemu utakuwa mji mtakatifu; na wageni hawatapita tena humo. “Wakati huo, milima itatiririka divai mpya, na vilima vitatiririka maziwa. Vijito vyote vya Yuda vitajaa maji; chemchemi itatokea nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu, na kulinywesha bonde la Shitimu. “Misri itakuwa mahame, Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu waliwashambulia watu wa Yuda wakawaua watu wasio na hatia. Bali Yuda itakaliwa milele, na Yerusalemu kizazi hata kizazi. Nitawaadhibu waliomwaga damu ya watu wa Yuda wala sitawaachia wenye hatia. Mimi, Mwenyezi-Mungu nakaa Siyoni.” Maneno ya Amosi, mmojawapo wa wachungaji wa mji wa Tekoa. Mungu alimfunulia Amosi mambo haya yote kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya lile tetemeko la ardhi, wakati Uzia alipokuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, alipokuwa mfalme wa Israeli. Amosi alisema hivi: Mwenyezi-Mungu ananguruma kutoka mlima Siyoni, anavumisha sauti yake kutoka Yerusalemu, hata malisho ya wachungaji yanakauka, nyasi mlimani Karmeli zinanyauka. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Damasko wametenda dhambi tena na tena; kwa hiyo, sitaacha kuwaadhibu; waliwatendea watu wa Gileadi ukatili mbaya. Basi, nitaishushia moto ikulu ya mfalme Hazaeli, nao utaziteketeza kabisa ngome za mfalme Ben-hadadi. Nitayavunjavunja malango ya mji wa Damasko, na kuwang'oa wakazi wa bonde la Aweni, pamoja na mtawala wa Beth-edeni. Watu wa Aramu watapelekwa uhamishoni Kiri. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Gaza wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Walichukua mateka watu kabila zima, wakawauza wawe watumwa kwa Waedomu. Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Gaza, nao utaziteketeza kabisa ngome zake. Nitawang'oa wakazi wa mji wa Ashdodi, pamoja na mtawala wa Ashkeloni. Nitanyosha mkono dhidi ya Ekroni, nao Wafilisti wote waliosalia wataangamia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Tiro wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Walichukua mateka kabila zima hadi Edomu, wakaukiuka mkataba wa urafiki waliokuwa wamefanya. Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Tiro, na kuziteketeza kabisa ngome zake.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Edomu wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Waliwawinda ndugu zao Waisraeli kwa mapanga, wakaitupilia mbali huruma yao yote ya kindugu. Hasira yao haikuwa na kikomo, waliiacha iwake daima. Basi, nitaushushia moto mji wa Temani, na kuziteketeza kabisa ngome za Bosra.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Amoni wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Katika vita vyao vya kupora nchi zaidi, waliwatumbua wanawake waja wazito nchini Gileadi. Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Raba, na kuziteketeza kabisa ngome zake. Siku hiyo ya vita patakuwa na makelele mengi, nayo mapambano yatakuwa makali kama tufani. Mfalme wao na maofisa wake, wote watakwenda kukaa uhamishoni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Moabu wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Wamemkosea heshima marehemu mfalme wa Edomu kwa kuichoma moto mifupa yake ili kujitengenezea chokaa! Basi, nitaishushia moto nchi ya Moabu, na kuziteketeza kabisa ngome za mji wa Keriothi. Wanajeshi watakapopaza sauti zao na kupiga tarumbeta, watu wa Moabu watakufa katika makelele hayo ya vita. Isitoshe, nitamuua mtawala wa Moabu, pamoja na viongozi wote wa nchi hiyo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Yuda wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Wamepuuza sheria zangu, wala hawakufuata amri zangu. Wamepotoshwa na miungu ileile waliyoihudumia wazee wao. Basi, nitaishushia moto nchi ya Yuda, na kuziteketeza kabisa ngome za Yerusalemu.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Waisraeli wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Wamewauza watu waaminifu kwa kuwa hawakuweza kulipa madeni yao; na kuwauza watu fukara wasioweza kulipa deni la kandambili. Huwanyanyasa na kuwakandamiza wanyonge, na maskini huwabagua wasipate haki zao. Mtu na baba yake hulala na mjakazi yuleyule, hivyo hulitia unajisi jina langu takatifu. Popote penye madhabahu, watu hulalia nguo walizotwaa kwa maskini kama dhamana ya madeni yao; na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai waliyotwaa kwa wadeni wao. “Hata hivyo, enyi watu wangu, kwa ajili yenu, niliwaangamiza kabisa Waamori ambao walikuwa wakubwa kama mierezi, wenye nguvu kama miti ya mialoni. Naam, niliwaangamiza, matawi na mizizi. Niliwatoeni kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza kupitia jangwani miaka arubaini, mpaka mkaichukua nchi ya Waamori kuwa yenu. Niliwateua baadhi ya wana wenu wawe manabii, na baadhi ya vijana wenu wawe wanadhiri. Je, enyi Waisraeli, haya nisemayo si ya kweli? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Lakini nyinyi mliwafanya wanadhiri wanywe divai, na kuwaamuru manabii wasitoe unabii. “Sasa basi, nitawagandamiza mpaka chini, kama gari lililojaa nafaka. Hata wapiga mbio hodari hawataweza kutoroka; wenye nguvu wataishiwa nguvu zao, na askari watashindwa kuyaokoa maisha yao. Wapiga upinde vitani hawatastahimili; wapiga mbio hodari hawataweza kujiokoa, wala wapandafarasi hawatayanusurisha maisha yao. Siku hiyo, hata askari hodari watatimua mbio bila chochote. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Enyi Waisraeli, sikilizeni neno Mwenyezi-Mungu alilosema dhidi yenu, enyi taifa zima alilolitoa nchini Misri: “Kati ya mataifa yote ulimwenguni, ni nyinyi tu niliowachagua. Kwa hiyo nitawaadhibu nyinyi, kwa sababu ya uovu wenu wote.” Je, watu wawili huanza safari pamoja, bila ya kufanya mpango pamoja kwanza? Je, simba hunguruma porini kama hajapata mawindo? Je, mwanasimba hunguruma pangoni mwake kama hajakamata kitu? Je, mtego bila chambo utamnasa ndege? Je, mtego hufyatuka bila kuguswa na kitu? Je, baragumu ya vita hulia mjini bila kutia watu hofu? Je, mji hupatwa na janga asilolileta Mungu? Hakika, Bwana Mwenyezi-Mungu hafanyi kitu bila kuwafunulia watumishi wake manabii nia yake. Simba akinguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana Mwenyezi-Mungu akinena, ni nani atakataa kuutangaza ujumbe wake? Tangazeni katika ikulu za Ashdodi, na katika ikulu za nchi ya Misri: “Kusanyikeni kwenye milima inayoizunguka nchi ya Samaria, mkajionee msukosuko mkubwa na dhuluma zinazofanyika humo.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu hawa wameyajaza majumba yao vitu vya wizi na unyang'anyi. Hawajui kabisa kutenda yaliyo sawa! Kwa hiyo, adui ataizingira nchi yao, atapaharibu mahali pao pa kujihami, na kuziteka nyara ikulu zao.” Mwenyezi-Mungu, asema hivi: “Kama vile mchungaji ampokonyavyo simba kinywani miguu miwili tu au kipande cha sikio la kondoo, ndivyo watakavyonusurika watu wachache tu wa Israeli wakaao Samaria, ambao sasa wanalalia vitanda vizuri na matandiko ya hariri.” Bwana Mungu wa majeshi asema hivi: “Sikilizeni, mkawaonye wazawa wa Yakobo: Siku nitakapowaadhibu Waisraeli kwa sababu ya makosa yao, nitayaharibu pia madhabahu ya mji wa Betheli. Nitazikata pembe za kila madhabahu na kuziangusha chini. Nitaziharibu nyumba zote mjini na vijijini; nitazibomoa nyumba zilizopambwa kwa pembe, majumba makubwamakubwa hayatasalia hata moja. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Sikilizeni neno hili, enyi wanawake ng'ombe wa Bashani mlioko huko mlimani Samaria; nyinyi mnaowaonea wanyonge, mnaowakandamiza maskini, na kuwaambia waume zenu: “Tuleteeni divai tunywe!” Sikilizeni ujumbe huu: Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu Mtakatifu nimeapa: “Tazama, siku zaja, ambapo watu watawakokoteni kwa kulabu, kila mmoja wenu kama samaki kwenye ndoana. Mtaburutwa hadi ukutani palipobomolewa, na kutupwa nje. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Enyi Waisraeli, nendeni basi huko Betheli mkaniasi! Nendeni Gilgali mkalimbikize makosa yenu! Toeni sadaka zenu kila asubuhi, na zaka zenu kila siku ya tatu. Toeni tambiko ya shukrani ya mikate iliyochachushwa. Tangazeni popote kwamba mmetoa kwa hiari; kwani ndivyo mnavyopenda kufanya! Mimi Bwana Mungu nimenena. “Mimi niliwanyima chochote cha kutafuna, nikasababisha ukosefu wa chakula popote. Hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Tena niliwanyima mvua miezi mitatu tu kabla ya mavuno. Niliunyeshea mvua mji mmoja, na mji mwingine nikaunyima. Shamba moja lilipata mvua, na lingine halikupata, likakauka. Watu wa miji miwili, mitatu wakakimbilia mji mwingine, wapate maji, lakini hayakuwatosha. Hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Niliwapiga pigo la ukame na ukungu; nikakausha bustani na mashamba yenu ya mizabibu; nzige wakala mitini na mizeituni yenu. Hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Niliwaleteeni ugonjwa wa tauni kama ule nilioupelekea Misri. Niliwaua vijana wenu vitani, nikawachukua farasi wenu wa vita. Maiti zilijaa katika kambi zenu, uvundo wake ukajaa katika pua zenu. Hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Niliwaangusha baadhi yenu kwa maangamizi kama nilivyoangamiza Sodoma na Gomora. Wale walionusurika miongoni mwenu, walikuwa kama kijiti kilichookolewa motoni. Hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Kwa hiyo, enyi Waisraeli, nitawaadhibu. Na kwa kuwa nitafanya jambo hilo, kaeni tayari kuikabili hukumu yangu!” Mungu ndiye aliyeifanya milima, na kuumba upepo; ndiye amjulishaye mwanadamu mawazo yake; ndiye ageuzaye mchana kuwa usiku, na kukanyaga vilele vya dunia. Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina lake! Sikilizeni maombolezo yangu juu yenu, enyi Waisraeli: Umeanguka na hutainuka tena ewe binti Israeli! Umeachwa pweke nchini mwako, hamna hata mtu wa kukuinua. Maana Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu 1,000 watatoka mjini kwenda kupigana lakini watarejea 100 tu; wataondoka watu 100 wa kijiji kimoja lakini watanusurika watu kumi tu.” Mwenyezi-Mungu awaambia hivi Waisraeli: “Nitafuteni mimi nanyi mtaishi! Lakini msinitafute huko Betheli wala msiende Gilgali wala msivuke kwenda Beer-sheba. Maana wakazi wa Gilgali, hakika watachukuliwa uhamishoni, na Betheli utaangamizwa!” Mtafuteni Mwenyezi-Mungu, nanyi mtaishi! La sivyo, atawalipukia wazawa wa Yosefu kama moto; moto utawateketeza wakazi wa Betheli na hakuna mtu atakayeweza kuuzima. Tahadhari enyi mnaogeuza haki kuwa uchungu, na kuuona uadilifu kuwa kama takataka! Huyo aliyezifanya Kilimia na sayari Orioni, ambaye huligeuza giza nene kuwa mchana, na mchana kuwa usiku; yeye ambaye ayaitaye pamoja maji ya bahari na kuyamwaga juu ya nchi kavu, Mwenyezi-Mungu ndilo jina lake. Yeye ndiye anayewaangamiza wenye nguvu, na kuziharibu ngome zao. Nyinyi huwachukia watetezi wa haki na wenye kusema ukweli mahakamani. Nyinyi mnawakandamiza fukara na kuwatoza kodi ya ngano kupita kiasi. Mnajijengea nyumba za mawe ya kuchonga, lakini nyinyi hamtaishi humo; mnalima bustani nzuri za mizabibu, lakini hamtakunywa divai yake. Maana mimi najua wingi wa makosa yenu na ukubwa wa dhambi zenu; nyinyi mnawatesa watu wema, mnapokea rushwa na kuzuia fukara wasipate haki mahakamani. Basi, kutakuwa na wakati mbaya ambao hata mwenye busara atanyamaza. Tafuteni kutenda mema na si mabaya, ili nyinyi mpate kuishi naye Mwenyezi-Mungu wa majeshi awe pamoja nanyi kama mnavyosema. Chukieni uovu, pendeni wema, na kudumisha haki mahakamani. Yamkini Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawafadhili watu wa Yosefu waliobaki. Basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, naam, Mwenyezi-Mungu asema: “Patakuwa na kilio kila mahali mitaani; watu wataomboleza: ‘Ole! Ole!’ Wakulima wataitwa waje kuomboleza, na mabingwa wa kuomboleza waje kufanya matanga. Patakuwa na kilio katika mashamba yote ya mizabibu; maana nitapita kati yenu kuwaadhibu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.” Ole wenu nyinyi mnaoingojea kwa hamu siku ya Mwenyezi-Mungu! Kwa nini mnaitaka sana siku hiyo? Siku hiyo, itakuwa siku ya giza na sio ya mwanga! Mambo yatakuwa kama mtu aliyekimbia simba, halafu akakumbana na dubu! Au kama mtu anayerudi nyumbani kwake, akatia mkono ukutani, akaumwa na nyoka. Siku ya Mwenyezi-Mungu itakuwa giza, na sio mwanga; itakuwa huzuni bila uangavu wowote. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nazichukia na kuzidharau sikukuu zenu; siifurahii mikutano yenu ya kidini. Mjaponitolea sadaka zenu za kuteketezwa na za nafaka, mimi sitakubali kuzipokea; na sadaka zenu za amani za wanyama wanono mimi sitaziangalia kabisa. Ondoeni mbele yangu kelele za nyimbo zenu! Sitaki kusikiliza muziki wa vinubi vyenu! Lakini acheni haki itiririke kama maji, uadilifu uwe kama mto usiokauka. “Enyi Waisraeli, wakati ule mlipokuwa kule jangwani kwa miaka arubaini, je, mliniletea tambiko na sadaka hata mara moja? Je, wakati huo mlibeba kama sasa vinyago vya mungu wenu Sakuthi mfalme wenu na vinyago vya Kaiwani mungu wenu wa nyota, vitu ambavyo mlijitengenezea wenyewe? Kwa hiyo nitawapeleka uhamishoni, mbali kuliko Damasko! Hayo amesema Mwenyezi-Mungu, ambaye jina lake ni Mungu wa Majeshi. Ole wenu nyinyi mnaostarehe huko Siyoni, nanyi mnaojiona salama mlimani Samaria! Nyinyi mwaonekana kuwa viongozi wa taifa maarufu ambao Waisraeli wote huwategemea. Haya! Nendeni Kalne mkaangalie kila mahali, tokeni huko mwende hadi mji ule mkubwa wa Hamathi, kisha teremkeni hadi Gathi kwa Wafilisti. Je, falme zao si bora kuliko zenu na eneo lao si bora kuliko lenu?” Nyinyi mnajaribu kuifukuza siku mbaya. Lakini mnauleta karibu utawala dhalimu. Ole wenu mnaolala juu ya vitanda vya pembe za ndovu na kujinyosha juu ya masofa, mkila nyama za wanakondoo na ndama! Nyinyi mnapenda kuimba ovyo na sauti ya vinubi na kubuni ala mpya za muziki mkimwiga mfalme Daudi. Mnakunywa divai kwa mabakuli, na kujipaka marashi mazuri mno. Lakini hamhuzuniki hata kidogo juu ya kuangamia kwa wazawa wa Yosefu. Kwa hiyo mtakuwa wa kwanza kwenda uhamishoni, na karamu za wenye kustarehe zitatoweka. Bwana Mwenyezi-Mungu ameapa kwa nafsi yake; Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi asema: “Nachukizwa mno na kiburi cha wazawa wa Yakobo; tena nayachukia majumba yao ya fahari. Mji wao na vyote vilivyomo nitawapa adui zao.” Kama wakibaki watu kumi katika nyumba moja, wote watakufa. Na atakapokuja mjomba wa aliyekufa kuitoa maiti nje aichome, akamwuliza yeyote atakayekuwako ndani pembeni mwa nyumba, “Je kuna mtu mwingine pamoja nawe?” Naye atamjibu, “La! Hamna!” Naye atamwambia, “Nyamaza kimya! Tusilitaje hata jina la Mwenyezi-Mungu.” Tazama! Mwenyezi-Mungu anatoa amri, nalo jumba kubwa labomoka vipandevipande, na nyumba ndogo kusagikasagika. Je, farasi waweza kupiga mbio miambani? Je, watu huilima bahari kwa ng'ombe? Lakini nyinyi mmeigeuza haki kuwa sumu, na tunda la uadilifu kuwa uchungu. Nyinyi mnashangilia juu ya Lodebari, na kusema mmeuteka Karnaimu kwa nguvu zenu wenyewe. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Enyi Waisraeli, kweli nitaleta taifa moja lije kuwashambulia, nalo litawatesa nyinyi kuanzia Lebo-hamathi kaskazini, hadi kijito cha Araba, upande wa kusini.” Siku moja, Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono: Nilimwona Mungu anaumba nzige kundi zima, mara baada ya watu kumaliza kukata nyasi kwa ajili ya wanyama wa mfalme. Wakati huo, nyasi zilikuwa ndio zinaanza kuchipua tena. Niliwaona nzige hao wakila na kumaliza kila jani katika nchi. Ndipo nikasema: “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi utuhurumie! Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi? Wao ni wadogo mno!” Basi, Bwana Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake, akasema, “Haitakuwa hivyo!” Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Nilimwona Bwana Mwenyezi-Mungu akiuita moto wa hukumu ya kuwaadhibu watu. Moto huo uliunguza vilindi vikuu vya bahari, ukaanza kuiteketeza nchi kavu. Ndipo nikasema: “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi uache kuadhibu! Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi? Wao ni wadogo mno!” Basi, Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake, akasema: “Hili pia halitatukia.” Mwenyezi-Mungu alinijalia tena maono mengine: Nilimwona Mwenyezi-Mungu amesimama karibu na ukuta, ameshika mkononi mwake uzi wenye timazi. Naye akaniuliza: “Amosi, unaona nini?” Nikamjibu, “Naona timazi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akasema: “Tazama! Naweka timazi kati ya watu wangu Waisraeli. Sitavumilia tena maovu yao. Huko vilimani ambako wazawa wa Isaka hutambikia, kutafanywa kuwa uharibifu mtupu na maskani ya Waisraeli yatakuwa magofu. Nitaushambulia kwa vita ukoo wa mfalme Yeroboamu.” Basi, Amazia kuhani wa mji wa Betheli, akampelekea mfalme Yeroboamu wa Israeli habari hizi: “Amosi analeta fitina juu yako katika ufalme wa Israeli. Hotuba zake ni hatari kwa nchi hii. Anachosema ni hiki: ‘Yeroboamu atakufa kwa upanga nao Waisraeli watapelekwa uhamishoni, mbali kabisa na nchi yao.’” Kisha Amazia akamwambia Amosi, “Sasa tumekuchoka, ewe nabii! Nenda zako! Rudi katika nchi ya Yuda, ukatoe unabii huko upate na ujira wako hukohuko. Usitoe tena unabii hapa mjini Betheli, kwa kuwa hapa ni maskani ya ibada ya mfalme; ni hekalu la utawala huu.” Amosi akamjibu Amazia, “Mimi si nabii wa kuajiriwa, wala si mmoja wa kikundi cha manabii. Mimi ni mchungaji na mtunza mikuyu. Mwenyezi-Mungu alinitoa katika kazi yangu hiyo ya uchungaji, akaniamuru nije kuwaambia unabii watu wake wa Israeli. Nawe basi, ewe Amazia, sikiliza neno la Mwenyezi-Mungu: Wewe waniambia nisitoe unabii dhidi ya Israeli, wala nisihubiri dhidi ya wazawa wa Isaka. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Mkeo atakuwa malaya mjini, na wanao wa kiume na kike watauawa vitani. Ardhi yako itagawanywa na kupewa wengine, nawe binafsi utafia katika nchi najisi, nao Waisraeli hakika watapelekwa uhamishoni, mbali kabisa na nchi yao.’” Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Niliona kikapu kilichojaa matunda ya kiangazi. Naye Mwenyezi-Mungu akaniuliza: “Amosi, unaona nini?” Nami nikamjibu, “Naona kikapu cha matunda ya kiangazi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Mwisho umewafikia watu wangu wa Israeli. Sitavumilia tena maovu yao. Siku hiyo, nyimbo za ikulu zitakuwa maombolezo. Kutakuwa na maiti nyingi, nazo zitatupwa nje kimyakimya.” Sikilizeni enyi mnaowakandamiza wanyonge na kuwaletea maangamizi fukara wa nchi. Mnajisemea mioyoni mwenu: “Sikukuu ya mwezi mwandamo itakwisha lini ili tuanze tena kuuza nafaka yetu? Siku ya Sabato itakwisha lini ili tupate kuuza ngano yetu? Tutatumia vipimo hafifu vya wastani na uzito, tutadanganya watu kwa mizani isizo sawa, hata kuuza ngano hafifu kwa bei kubwa. Tutaweza kununua watu fukara kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya kandambili.” Mwenyezi-Mungu, fahari ya Yakobo, ameapa: “Hakika, sitayasahau matendo yao maovu. Kwa hiyo, dunia itatetemeka na kila mtu nchini ataomboleza. Nchi yote itayumbayumba; itapanda na kushuka, kama yanavyojaa na kupwa maji ya mto Nili!” Bwana Mwenyezi-Mungu asema, “Siku hiyo nitalifanya jua litue adhuhuri, na kuijaza nchi giza mchana. Sherehe zenu nitazigeuza kuwa kilio, na nyimbo zenu za furaha kuwa maombolezo. Nitawafanya nyote mvae magunia kwa huzuni na kunyoa vipara vichwa vyenu, kama kuomboleza kifo cha mtoto wa pekee; na siku ya mwisho itakuwa ya uchungu mkubwa.” Bwana Mwenyezi-Mungu asema, “Siku zaja ambapo nitaleta njaa nchini. Lakini sio njaa na kiu ya chakula na maji, bali njaa ya kusikia maneno ya Mwenyezi-Mungu. Watu watatangatanga kutoka bahari hata bahari, kutoka upande wa kaskazini mpaka mashariki. Watakimbia huko na huko wakitafuta neno la Mwenyezi-Mungu, lakini hawatalipata. “Siku hiyo, hata vijana wenye afya, wa kiume kwa wa kike, watazimia kwa kiu. Wale wanaoapa kwa mungu wa uongo wa Samaria, na kusema: ‘Kwa nafsi ya mungu wako ee Dani’; na, ‘Kwa nafsi ya mungu wa Beer-sheba’, wote wataanguka na hawatainuka tena kamwe.” Nilimwona Mwenyezi-Mungu amesimama kando ya madhabahu, naye akaniamuru: “Zipige hizo nguzo za hekalu mpaka misingi yake itikisike. Zivunje hizo nguzo ziwaangukie watu vichwani. Wale watakaosalia nitawaua kwa upanga; hakuna hata mmoja wao atakayenusurika, naam, hakuna atakayetoroka. Wajapojichimbia njia ya kwenda kuzimu, huko nitawachukua kwa mkono wangu; wajapopanda mbinguni, nitawaporomosha chini. Wajapojificha juu ya mlima Karmeli, huko nitawasaka na kuwachukua; wajapojificha mbali nami vilindini mwa bahari, humo nitaliamuru joka la baharini liwaume. Wajapochukuliwa mateka na adui zao, huko nitatoa amri wauawe kwa upanga. Nitawachunga kwa makini sana niwatendee mabaya na si mema.” Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, anaigusa ardhi nayo inatetemeka na wakazi wake wanaomboleza; dunia nzima inapanda na kushuka kama kujaa na kupwa kwa mto Nili wa Misri. Mwenyezi-Mungu amejenga makao yake mbinguni, nayo dunia akaifunika kwa anga; huyaita maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya nchi kavu. Mwenyezi-Mungu, ndilo jina lake! Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kwangu mimi, nyinyi Waisraeli, hamna tofauti yoyote na watu wa Kushi! Niliwatoa Wafilisti kutoka Krete, na Waashuru kutoka Kiri, kama nilivyowatoa nyinyi kutoka Misri. Mimi, Bwana Mwenyezi-Mungu nautazama ufalme wenye dhambi, na nitauangamiza kabisa kutoka duniani. Lakini sitawaangamiza wazawa wote wa Yakobo. “Tazama, nitatoa amri, na kuwapepeta Waisraeli kati ya mataifa kama mtu achekechavyo nafaka niwakamate wote wasiofaa. Wenye dhambi miongoni mwa watu wangu, watafia vitani kwa upanga; hao ndio wasemao: ‘Maafa hayatatukumba wala kutupata!’ “Siku yaja nitakapoisimika nyumba ya Daudi iliyoanguka; nitazitengeneza kuta zake, na kusimika upya magofu yake. Nitaijenga upya kama ilivyokuwa hapo zamani. Nao Waisraeli watamiliki mabaki ya Edomu na mataifa yote yaliyokuwa yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema, na nitafanya hivyo. “Wakati waja kwa hakika, ambapo mara baada ya kulima mavuno yatakuwa tayari kuvunwa; mara baada ya kupanda mizabibu utafuata wakati wa kuvuna zabibu. Milima itabubujika divai mpya, navyo vilima vitatiririka divai. Nitarekebisha hali ya watu wangu Waisraeli. Watajenga miji yao iliyoharibiwa na kuishi humo; watapanda mizabibu na kunywa divai yake; watalima mashamba na kula mazao yake. Nitawasimika katika nchi yao, wala hawatang'olewa tena kutoka katika nchi niliyowapa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Maono ya Obadia. Mambo aliyosema Bwana Mwenyezi-Mungu kuhusu taifa la Edomu. Tumepata habari kutoka kwa Mwenyezi-Mungu; mjumbe ametumwa kati ya mataifa: “Inukeni! Twende tukapigane na Edomu!” Mwenyezi-Mungu aliambia taifa la Edomu: “Nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa, utadharauliwa kabisa na wote. Kiburi chako kimekudanganya: Kwa kuwa mji wako mkuu ni ngome ya miamba imara na makao yako yapo juu milimani, hivyo wajisemea, ‘Nani awezaye kunishusha chini?’ Hata ukiruka juu kama tai, ukafanya makao yako kati ya nyota, mimi nitakushusha chini tu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Kama wezi au wanyang'anyi wangekujia usiku, je, wasingechukua tu kiasi cha kuwatosha? Ikiwa wavunaji zabibu wangekujia, je, wasingekuachia kiasi kidogo tu? Lakini wewe, adui zako wamekuangamiza kabisa. Enyi wazawa wa Esau, mali zenu zimetekwa; hazina zenu zote zimeporwa! Washirika wenzenu wamewadanganya, wamewafukuza nchini mwenu. Mliopatana nao wamewashinda vitani, rafiki wa kutegemewa ndio waliokutegea mitego, nawe hukuelewa yaliyokuwa yanatendeka. Mimi Mwenyezi-Mungu nakuuliza hivi: Je, siku hiyo, sitawaangamiza wenye hekima kutoka Edomu na wenye maarifa kutoka mlima Esau? Ewe Temani, mashujaa wako watatishika na kila mtu atauawa mlimani Esau. “Kwa sababu ya matendo maovu mliyowatendea ndugu zenu wazawa wa Yakobo, mtaaibishwa na kuangamizwa milele. Siku ile mlisimama kando mkitazama tu, wakati wageni walipopora utajiri wao, naam, wageni walipoingia malango yao na kugawana utajiri wa Yerusalemu kwa kura. Kwa hiyo nanyi mlitenda kama wazawa wao. Msingalifurahia siku hiyo ndugu zenu walipokumbwa na mikasa; msingaliwacheka Wayuda na kuona fahari wakati walipoangamizwa; msingalijigamba wenzenu walipokuwa wanataabika. Msingeliingia katika mji wa watu wangu, siku walipokumbwa na maafa; msingelipora mali zao, siku hiyo ya maafa yao. Msingelisimama kwenye njia panda na kuwakamata wakimbizi wao; wala msingeliwakabidhi kwa adui zao wale waliobaki hai. “Siku inakaribia ambapo mimi Mwenyezi-Mungu nitayahukumu mataifa yote. Kama mlivyowatendea wengine, ndivyo mtakavyotendewa, mtalipwa kulingana na matendo yenu. Maana, kama walivyokunywa kikombe cha ghadhabu yangu kwenye mlima wangu mtakatifu ndivyo na mataifa jirani yatakavyokunywa; watakunywa na kupepesuka, wataangamia kana kwamba hawakuwahi kuwapo duniani. “Lakini mlimani Siyoni watakuwapo wale waliosalimika nao utakuwa mlima mtakatifu. Wazawa wa Yakobo wataimiliki tena nchi iliyokuwa yao. Wazawa wa Yakobo watakuwa kama moto na wazawa wa Yosefu kama miali ya moto. Watawaangamiza wazawa wa Esau kama vile moto uteketezavyo mabua makavu, asinusurike hata mmoja wao. Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema. Wale wanaokaa Negebu wataumiliki mlima Esau; wale wanaokaa Shefela wataimiliki nchi ya Wafilisti. Waisraeli watamiliki nchi za Efraimu na Samaria na watu wa Benyamini wataimiliki nchi ya Gileadi. Waisraeli walio uhamishoni Hala wataimiliki Foinike hadi Sarepta. Watu wa Yerusalemu walio uhamishoni Sefaradi wataimiliki miji ya Negebu. Waokoaji watapanda juu ya mlima Siyoni ili kuutawala mlima Esau; naye Mwenyezi-Mungu atakuwa ndiye Mfalme.” Siku moja, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yona, mwana wa Amitai: “Ondoka uende Ninewi, ule mji mkuu, ukaukemee, maana nimeona uovu wake ni mkubwa mno.” Basi, Yona akaanza safari, lakini akashika njia ya kwenda Tarshishi ili kumkwepa Mwenyezi-Mungu. Akaenda hadi mjini Yopa ambapo alikuta meli moja iko tayari kwenda Tarshishi. Alilipa nauli, akapanda meli, akasafiri na mabaharia hao kwenda Tarshishi ili kumkwepa Mwenyezi-Mungu. Lakini Mwenyezi-Mungu akavumisha upepo mkali baharini, ikatokea dhoruba kali, meli ikawa karibu kabisa kuvunjika. Mabaharia wakajawa na hofu, kila mmoja akaanza kumlilia mungu wake; wakatupa baharini shehena ya meli ili kupunguza uzito wake. Wakati huo, Yona alikuwa ameteremkia sehemu ya ndani ya meli, akawa amelala usingizi mzito. Nahodha akamwendea, akamwambia, “Wawezaje wewe kulala? Amka umwombe Mungu wako; labda Mungu wako atatuhurumia, tusiangamie.” Mabaharia wakasemezana: “Tupige kura tujue balaa hili limetupata kwa kosa la nani.” Basi, wakapiga kura; kura ikamwangukia Yona. Hapo wakaanza kumhoji: “Haya, sasa tuambie! Kwa nini balaa hili linatupata? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? U kabila gani?” Yona akawajibu, “Mimi ni Mwebrania; namcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, muumba wa bahari na nchi kavu.” Kisha Yona akawaeleza kwamba alikuwa anamkwepa Mwenyezi-Mungu. Kusikia hayo, mabaharia hao wakazidi kujawa na hofu, wakamwambia, “Umefanya nini wewe!” Wakati huo wote, bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Basi, wakamwuliza Yona, “Tukufanye nini ili bahari itulie?” Yona akawajibu, “Nichukueni mkanitupe baharini, nayo bahari itatulia, maana naona wazi kwamba dhoruba hii imewapata kwa sababu yangu mimi.” Mabaharia hao wakajaribu bado kupiga makasia wapate kuifikisha meli yao pwani, lakini hawakufanikiwa kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia. Basi, wakamlilia Mwenyezi-Mungu wakisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, twakusihi usituangamize kwa kuutoa uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa kumwaga damu ya mtu asiye na hatia. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umefanya upendavyo.” Basi, wakamchukua Yona, wakamtupa baharini, na papo hapo bahari ikatulia. Mabaharia hao wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu, wakamtolea sadaka na kuweka nadhiri. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaamuru samaki mkubwa ammeze Yona, naye akawa tumboni mwa samaki huyo kwa muda wa siku tatu, usiku na mchana. Basi, Yona, akiwa tumboni mwa samaki huyo, akawa akimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akisema: “Kwa sababu ya taabu yangu, nilikuomba, ee Mwenyezi-Mungu, nawe ukanisikiliza; toka chini kuzimu, nilikulilia, nawe ukasikiliza kilio changu. Ulinitupa katika kilindi, katikati ya bahari, gharika ikanizunguka, mawimbi na gharika vikapita juu yangu. Nilidhani kwamba nimetengwa nisiwe mbele yako; nisiweze kuliona tena hekalu lako takatifu. Maji yalinizunguka na kunisonga; kilindi kilinifikia kila upande, majani ya baharini yakanifunika kichwa. Niliteremka hadi kwenye misingi ya milima, katika nchi ambayo milango yake imefungwa milele. Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umenipandisha hai kutoka humo shimoni. Roho yangu ilipoanza kunitoka, nilikukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu, sala yangu ikakufikia, katika hekalu lako takatifu. Watu wanaoabudu sanamu za miungu batili, huutupilia mbali uaminifu wao kwako. Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani, nitakutolea sadaka, na kutimiza nadhiri zangu. Mwenyezi-Mungu, ndiye aokoaye.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamwamuru yule samaki, naye akamtapika Yona kwenye nchi kavu. Neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yona mara ya pili: “Nenda Ninewi, ule mji mkuu, ukawatangazie watu ujumbe niliokupa.” Basi, Yona akaondoka, akaenda Ninewi kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza. Mji wa Ninewi ulikuwa mkubwa sana. Upana wake ulikuwa mwendo wa siku tatu. Alipowasili, Yona aliingia mjini, na baada ya kutembea mwendo wa siku nzima, akaanza kutangaza: “Bado siku arubaini tu na mji huu wa Ninewi utaangamizwa!” Basi, watu wa Ninewi wakauamini ujumbe wa Mungu, wakatangaza mfungo, na kwamba kila mmoja wao, mkubwa kwa mdogo, avae vazi la gunia kama ishara ya kutubu. Habari hizi zikamfikia mfalme wa Ninewi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake rasmi, akajivika vazi la gunia na kuketi katika majivu. Kisha mfalme akawatangazia wakazi wa Ninewi: “Mimi mfalme, pamoja na wakuu wangu, natoa amri hii: Pasiwe na binadamu yeyote, ng'ombe au mnyama yeyote wa kufugwa, atakayeonja kitu chochote. Ni mwiko kwa mtu yeyote au mnyama kula au kunywa. Watu wote na wanyama wavae mavazi ya gunia. Kila mtu na amwombe Mungu na kumsihi kwa moyo. Naam, kila mmoja na aache uovu na ukatili wake. Huenda Mungu akabadili nia yake, akaacha kutukasirikia, tusije tukaangamia!” Mungu alipoona walivyofanya, na jinsi walivyouacha uovu wao, akabadili nia yake, akaacha kuwatenda kama alivyokuwa amekusudia. Lakini jambo hilo halikumpendeza Yona hata kidogo, akakasirika sana. Kwa hiyo akaomba, “Mwenyezi-Mungu, je, hayo si mambo yaleyale niliyowaza utayafanya nilipokuwa nyumbani? Ndio maana nilifanya haraka kukimbilia Tarshishi. Nilijua kwamba wewe u Mungu wa upendo na huruma. Hukasiriki upesi, daima u mwema na u tayari kubadili nia yako wakati wowote ili usiadhibu. Basi, sasa ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi uniondolee uhai wangu, maana, kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kuishi.” Naye Mwenyezi-Mungu akamjibu Yona: “Unadhani wafanya vema kukasirika?” Ndipo Yona akatoka nje ya mji, akajikalia upande wa mashariki wa mji huo. Hapo, akajijengea kibanda, akaketi kivulini mwake huku anangojea apate kuona litakaloupata mji wa Ninewi. Mungu, Mwenyezi-Mungu akaamuru mmea uote na kukua. Akauotesha ili kumpatia Yona kivuli cha kumpunguzia taabu aliyokuwa nayo. Yona akaufurahia sana mmea huo. Lakini siku ya pili, kulipopambazuka, Mungu akaamuru mdudu auharibu mmea huo, ukanyauka. Jua lilipochomoza, Mungu akaleta upepo wa hari kutoka mashariki, jua likamchoma sana Yona kichwani, karibu azirai. Yona akasema, “Afadhali kufa kuliko kuishi!” Lakini Mungu akamwambia Yona, “Je, unadhani wafanya vema kuukasirikia mmea huo?” Yona akajibu, “Ndiyo, nafanya vema kukasirika — kukasirika hata kufa!” Hapo Mungu akamwambia, “Mmea huu uliota na kukua kwa usiku mmoja, na usiku uliofuata ukanyauka. Wewe hukuufanyia kitu chochote, wala hukuuotesha. Mbona unauhurumia? Je, haifai kwangu kuuhurumia mji wa Ninewi, ule mji mkuu wenye watu 120,000, wasioweza kupambanua jema na baya, na pia wanyama wengi?” Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Mika, mwenyeji wa Moreshethi, wakati Yothamu, Ahazi na Hezekia walipokuwa wafalme wa Yuda. Mika aliona mambo yote haya kuhusu Samaria na Yerusalemu. Sikilizeni enyi watu wote; sikiliza ewe dunia na vyote vilivyomo. Mwenyezi-Mungu anakuja kuwashtaki, Bwana anena kutoka hekalu lake takatifu. Naam! Mwenyezi-Mungu yuaja kutoka makao yake; atashuka na kutembea juu ya vilele vya dunia. Milima itayeyuka chini ya nyayo zake, kama nta karibu na moto; mabonde yatapasuka, kama maji yaporomokayo kwenye mteremko. Haya yote yatatukia kwa sababu ya makosa ya wazawa wa Yakobo, kwa sababu ya dhambi za wazawa wa Israeli. Je, uhalifu wa Yakobo waonekana wapi? Katika mji wake mkuu Samaria! Je, uhalifu wa Yuda waonekana wapi? Katika Yerusalemu kwenyewe! Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mji wa Samaria nitaufanya magofu nyikani, shamba ambalo watu watapanda mizabibu. Mawe yaliyoujenga nitayatupa bondeni, na misingi yake nitaichimbuachimbua. Sanamu zake zote zitavunjwavunjwa, kila kilichochumwa kitateketezwa kwa moto. Vinyago vyake vyote nitaviharibu. Vilirundikwa kutokana na ujira wa malaya, navyo vitatumiwa tena kulipia umalaya.” Kwa sababu hiyo, mimi nitalia na kuomboleza; nitatembea uchi na bila viatu. Nitaomboleza na kulia kama mbweha, nitasikitika na kulia kama mbuni. Majeraha ya Samaria hayaponyeki, nayo yameipata pia Yuda; yamefikia lango la Yerusalemu, mahali wanapokaa watu wangu. Msiitangaze habari hii huko Gathi, wala msilie machozi! Huko Beth-leafra mgaegae mavumbini kwa huzuni. Nendeni enyi wakazi wa Shafiri, mkiwa uchi na wenye haya. Wakazi wa Zaanani msitoke nje ya mji wenu. Watu wa Beth-ezeli wanalia; msaada wao kwenu umeondolewa. Wakazi wa Marothi wanangojea msaada kwa hamu kubwa, lakini maangamizi yaja kutoka kwa Mwenyezi-Mungu karibu kabisa na lango la Yerusalemu. Enyi wakazi wa Lakishi, fungeni farasi wepesi na magari ya vita. Nyinyi mlikuwa mmeiga dhambi ya watu wa Siyoni, makosa ya Waisraeli yalikuwa kwenu. Hivyo, mnapaswa kuagana na kuwaacha wakazi wa Morasheth-gathi. Nao mji wa Akzibu hautawasaidia wafalme wa Israeli, Enyi wakazi wa Maresha, Mungu atawaleteeni tena adui atakayewateka. Viongozi waheshimiwa wa Israeli watakimbilia pangoni huko Adulamu. Enyi watu wa Yuda, nyoeni upara kuwaombolezea watoto wenu wapenzi; panueni upara wenu uwe mpana kama wa tai, maana watoto wenu watawaacha kwenda uhamishoni. Ole wao wanaopanga kutenda maovu wanaolala usiku wakiazimia uovu! Mara tu kunapopambazuka, wanayatekeleza kwani wanao uwezo. Hutamani mashamba na kuyatwaa; wakitaka nyumba, wananyakua. Huwadhulumu wenye nyumba na jamaa zao, huwanyang'anya watu mali zao. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ninapanga kuwaleteeni nyinyi maafa, ambayo kamwe hamtaweza kuyakwepa. Utakuwa wakati mbaya kwenu, wala hamtaweza kwenda kwa maringo. Siku hiyo watu watawasimanga kwa wimbo, watalia na kuomboleza kwa uchungu, wakisema: ‘Tumeangamia kabisa; Mwenyezi-Mungu amechukua nchi yetu, naam, ameiondoa mikononi mwetu. Mashamba yetu amewagawia waliotuteka.’” Kwa hiyo hamtagawiwa sehemu yoyote ya ardhi miongoni mwa watu wake Mwenyezi-Mungu. “Usituhubirie sisi. Mambo kama hayo si ya kuhubiriwa. Sisi hatutakumbwa na maafa! Je, yafaa kusema hivyo, wazawa wa Yakobo? Je, Mwenyezi-Mungu ameacha uvumilivu wake? Je, yeye hufanya mambo kama haya?” Sivyo! Maneno yangu huwafaa watendao mambo mema. Lakini Mwenyezi-Mungu awaambia hivi: “Nyinyi mnawavamia watu wangu kama adui. Mnawanyang'anya mavazi yao watu watulivu; watu wanaopita kwenda zao bila wasiwasi, na wasio na fikira zozote za vita. Mnawafukuza wake za watu wangu kutoka nyumba zao nzuri; watoto wao mmewaondolea fahari yangu milele. Inukeni mwende zenu! Hapa hamna tena pa kupumzika! Kwa utovu wenu wa uaminifu maangamizi makubwa yanawangojea! Kama mtu angetokea akatamka maneno matupu ya uongo na kusema: ‘Nawatabirieni divai na pombe kwa wingi’, mhubiri wa namna hiyo angependwa na watu hawa! “Lakini kweli nitawakusanya nyote enyi watu wa Yakobo, naam, nitawakusanya enyi Waisraeli mliobaki, niwalete pamoja kama kondoo katika zizi, kama kundi kubwa la kondoo malishoni; nanyi mtakuwa kundi la watu wengi.” Yule atakayetoboa njia atawatangulia, nao watalivunja lango la mji na kutoka nje, watapita na kutoka nje. Mfalme wao atawatangulia; Mwenyezi-Mungu mwenyewe atawatangulia. Sasa sikilizeni enyi wakuu wa wazawa wa Yakobo, sikilizeni, enyi watawala wa wazawa wa Israeli! Nyinyi ndio mnaopaswa kujua mambo ya haki. Lakini nyinyi mnachukia mema na kupenda maovu. Mnawachuna ngozi watu wangu, na kubambua nyama mifupani mwao. Mnajilisha kwa nyama ya watu wangu mnawachuna ngozi yao, mnaivunjavunja mifupa yao, na kuwakatakata kama nyama ya kupika, kama nyama ya kutia ndani ya chungu. Wakati unakuja ambapo mtamlilia Mwenyezi-Mungu, lakini yeye hatawajibu. Atauficha uso wake wakati huo, kwa sababu mmetenda mambo maovu. Mwenyezi-Mungu asema hivi kuhusu manabii wanaowapotosha watu wake; manabii ambao hutabiri amani wakipewa kitu, lakini huwatishia watu kwa vita wasipopewa kitu: “Kwenu manabii kutakuwa usiku bila maono, kutakuwa giza kwenu bila ufunuo. Kwenu manabii kutakuchwa, mchana utakuwa giza kwenu.” Mabingwa wa maono watafedheheka, mafundi wa kubashiri wataaibishwa; wote watafunga midomo yao, maana hawatapata jibu lolote kutoka kwa Mungu. Lakini kwa upande wangu, nimejazwa nguvu na roho ya Mwenyezi-Mungu; nimejaliwa kujua haki na kuwa na uwezo niwatangazie wazawa wa Yakobo kosa lao, niwaambie Waisraeli dhambi yao. Sikieni jambo hili enyi viongozi wa wazawa wa Yakobo, sikilizeni, enyi watawala wa Waisraeli: Nyinyi mnachukia mambo ya haki na kupotosha mambo ya adili. Nyinyi mnajenga mji wa Siyoni kwa damu, naam, mji wa Yerusalemu kwa dhuluma. Waamuzi hufanya kazi yao kwa rushwa, makuhani wake hufundisha kwa malipo, manabii hutabiri kwa fedha. Hata hivyo hujidai kumtegemea Mwenyezi-Mungu, wakisema, “Mwenyezi-Mungu, si yupo pamoja nasi? Hatutapatwa na madhara yoyote!” Haya! Kwa sababu yenu, Siyoni utalimwa kama shamba, Yerusalemu utakuwa magofu, nao mlima wa hekalu utakuwa msitu. Utakuja wakati ambapo mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu utakuwa mkubwa kuliko milima yote. Naam, utakwezwa juu ya vilima vyote. Watu wengi watamiminika huko, mataifa mengi yataujia na kusema: “Twendeni juu kwenye mlima wa Mwenyezi-Mungu, twende katika nyumba ya Mungu wa Yakobo, ili atufundishe njia zake, nasi tufuate nyayo zake. Maana mwongozo utatoka huko Siyoni; neno la Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu.” Mungu atasuluhisha mizozo ya mataifa mengi, atakata mashauri ya mataifa makubwa ya mbali. Nayo yatafua mapanga yao kuwa majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kupogolea. Taifa halitapigana na taifa lingine, wala hayatafanya tena mazoezi ya vita. Kila mtu atakaa kwa amani chini ya mitini na mizabibu yake, bila kutishwa na mtu yeyote. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ametamka yeye mwenyewe. Mataifa mengine hufuata njia zao, kwa kuitegemea miungu yao, lakini sisi twafuata njia zetu kwa kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, milele na milele. Mwenyezi-Mungu asema, “Siku ile nitawakusanya walemavu, naam, nitawakusanya waliochukuliwa uhamishoni, watu wale ambao niliwaadhibu. Hao walemavu ndio watakaobaki hai; hao waliochukuliwa uhamishoni watakuwa taifa lenye nguvu. Nami Mwenyezi-Mungu nitawatawala mlimani Siyoni, tangu wakati huo na hata milele.” Nawe kilima cha Yerusalemu, wewe ngome ya Siyoni, ambamo Mungu anafanya ulinzi juu ya watu wake, kama mchungaji juu ya kondoo wake; wewe utakuwa tena mji maarufu kama hapo awali, Yerusalemu utakuwa tena mji mkuu wa mfalme. Sasa kwa nini mnalia kwa sauti? Je, hamna mfalme tena? Mshauri wenu ametoweka? Mnapaza sauti ya uchungu, kama mama anayejifungua! Enyi watu wa Siyoni, lieni na kugaagaa kama mama anayejifungua! Maana sasa mtaondoka katika mji huu mwende kukaa nyikani, mtakwenda mpaka Babuloni. Lakini huko, mtaokolewa. Huko Mwenyezi-Mungu atawakomboa makuchani mwa adui zenu. Mataifa mengi yamekusanyika kuwashambulia. Yanasema: “Acheni mji wao utiwe najisi, nasi tuyaone magofu ya Siyoni!” Lakini wao hawafahamu mawazo ya Mwenyezi-Mungu wala hawaelewi mpango wake: Kwamba amewakusanya pamoja, kama miganda mahali pa kupuria. Mwenyezi-Mungu asema, “Enyi watu wa Siyoni, inukeni mkawaadhibu adui zenu! Nitawapeni nguvu kama fahali mwenye pembe za chuma na kwato za shaba. Mtawasaga watu wa mataifa mengi; mapato yao mtaniwekea wakfu mimi, mali zao mtanitolea mimi Bwana wa dunia yote.” Jumuikeni mkajikusanye enyi watu wa Yerusalemu; mkisema: “Tumezingirwa, tumesongwa; naye kiongozi wa Israeli wanampiga shavuni kwa fimbo.” Mwenyezi-Mungu asema, “Lakini wewe Bethlehemu katika Efratha, wewe ni mdogo tu kati ya jamii za Yuda, lakini kwako kutatoka mtawala atakayetawala juu ya Israeli kwa niaba yangu. Asili yake ni ya zama za kale.” Hivyo Mungu atawaacha watu wake kwa maadui, mpaka yule mama mjamzito atakapojifungua. Kisha ndugu zake waliobakia, watarudi na kuungana na Waisraeli wenzao. Huyo mtawala atawachunga watu wake kwa nguvu ya Mwenyezi-Mungu, kwa fahari yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. Watu wake wataishi kwa usalama, maana atakuwa mkuu mpaka miisho ya dunia. Yeye ndiye atakayeleta amani. Waashuru wakivamia nchi yetu, na kuupenya ulinzi wetu, tutapeleka walinzi wawakabili, naam, tutawapeleka viongozi wetu kwa wingi. Kwa silaha zao wataitawala nchi ya Ashuru, na kuimiliki nchi ya Nimrodi. Watatuokoa mikononi mwa Waashuru, watakapowasili mipakani mwa nchi yetu na kuanza kuivamia nchi yetu. Wazawa wa Yakobo watakaobaki hai wameenea miongoni mwa mataifa mengi, watakuwa kama umande wa Mwenyezi-Mungu uburudishao, kama manyunyu yaangukayo penye nyasi ambayo hayasababishwi na mtu wala kumtegemea binadamu. Wazawa wa Yakobo watakaobaki hai, wameenea miongoni mwa mataifa na watu wengi watakuwa na nguvu kubwa kama simba kati ya wanyama wa porini, kama mwanasimba miongoni mwa makundi ya kondoo, ambaye kila mahali apitapo, huyarukia na kuyararua mawindo yake, asiwepo mtu yeyote wa kuyaokoa. Waisraeli watawashinda adui zao na kuwaangamiza kabisa. Mwenyezi-Mungu asema, “Wakati huo nitawaondoa farasi wenu, na kuyaharibu magari yenu ya farasi. Nitaiharibu miji ya nchi yenu, na kuzibomolea mbali ngome zenu. Nitatokomeza matendo yenu ya uchawi, nanyi hamtakuwa tena na wapiga ramli. Nitaziharibu sanamu zenu, na nguzo zenu za ibada; nanyi mtakoma kuabudu vitu mlivyotengeneza wenyewe. Nitazing'oa sanamu za Ashera kutoka kwenu, na kuiangamiza miji yenu. Kwa hasira na ghadhabu yangu, nitalipiza kisasi mataifa yote yasiyonitii.” Sikilizeni anachosema Mwenyezi-Mungu: “Wewe nabii, nenda ukailalamikie milima, navyo vilima visikie sauti yako.” Sikilizeni kesi ya Mwenyezi-Mungu enyi milima, sikilizeni enyi misingi ya kudumu ya dunia! Mwenyezi-Mungu anayo kesi dhidi ya watu wake. Yeye atatoa mashtaka dhidi ya Waisraeli. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wangu, nimewatendea nini? Nimewachosha kwa kitu gani? Nijibuni! Mimi niliwatoa nchini Misri; niliwakomboa kutoka utumwani; niliwapeni Mose, Aroni na Miriamu kuwaongoza. Enyi watu wangu, kumbukeni njama za Balaki mfalme wa Moabu, na jinsi Balaamu mwana wa Beori alivyomjibu. Kumbukeni yaliyotukia njiani kati ya Shitimu na Gilgali. Kumbukeni mtambue matendo yangu ya kuwaokoa!” Nimwendee Mwenyezi-Mungu na kitu gani, nipate kumwabudu Mungu aliye juu? Je, nimwendee na sadaka za kuteketezwa, nimtolee ndama wa mwaka mmoja? Je, Mwenyezi-Mungu atapendezwa nikimtolea maelfu ya kondoo madume, au mito elfu na elfu ya mafuta? Je, nimtolee mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu, naam, mtoto wangu kwa ajili ya dhambi yangu? Mungu amekuonesha yaliyo mema, ewe mtu; anachotaka Mwenyezi-Mungu kwako ni hiki: Kutenda mambo ya haki, kupenda kuwa na huruma, na kuishi kwa unyenyekevu na Mungu wako. Mwenyezi-Mungu anawaita wakazi wa mji, na ni jambo la busara sana kumcha yeye: “Sikilizeni, enyi watu wa Yuda; sikilizeni enyi mliokusanyika mjini. “Je, nitavumilia maovu yaliyorundikwa nyumbani mwao, mali zilizopatikana kwa udanganyifu, na matumizi ya mizani danganyifu, jambo ambalo ni chukizo? Je, naweza kusema hawana hatia watu wanaotumia mizani ya danganyifu na mawe ya kupimia yasiyo halali? Matajiri wa miji wamejaa dhuluma, wakazi wake husema uongo, kila wasemacho ni udanganyifu. Kwa hiyo nami, nimeanza kuwaangusha chini, na kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu. Mtakula lakini hamtashiba; ndani mwenu njaa itazidi kuwauma. Mkiweka akiba haitahifadhiwa, na mkihifadhi kitu nitakiharibu kwa vita. Mtapanda mbegu, lakini hamtavuna. Mtasindika zeituni, lakini hamtatumia hayo mafuta. Mtasindika zabibu, lakini hamtakunywa hiyo divai. Nyinyi mnafuata mfano mbaya wa mfalme Omri na mfano wa jamaa ya mfalme Ahabu na mfano mbaya wa jamaa ya mwanawe, Ahabu, na mmefuata mashauri yao. Kwa hiyo nitawaleteeni maangamizi, na kila mtu atawadharau. Watu watawadhihaki kila mahali.” Ole wangu! Hali ilivyo ni kama baada ya mavuno; hakuna tini za mwanzoni ninazotamani. Ni kama wakati wa kuchuma zabibu hakuna hata shada moja la zabibu la kula! Hakuna mcha Mungu aliyebaki nchini, hakuna mtu yeyote mnyofu miongoni mwa watu. Kila mmoja anavizia kumwaga damu; kila mmoja anamwinda mwenzake amnase. Wote ni mabingwa wa kutenda maovu; viongozi na mahakimu hutaka rushwa. Wakubwa huonesha wazi nia zao mbaya, na kufanya hila kuzitekeleza. Mwema zaidi kati yao hutaabisha kama mbigili, aliye mnyofu zaidi ni kama ua wa miiba. Siku iliyongojewa ya adhabu yao imefika. Na sasa mahangaiko yamewakumba. Usimwamini mwenzako, wala usimtumainie rafiki yako. Chunga unachosema kwa mdomo wako, hata na mke wako wewe mwenyewe. Maana, mtoto wa kiume anamdharau baba yake; mtoto wa kike anashindana na mama yake, mke wa mwana anapingana na mama mkwe wake. Maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake. Lakini mimi namtumainia Mwenyezi-Mungu, namtazamia Mungu mwenye kuniokoa; Mungu wangu atanisikiliza. Usifurahie maafa yangu ewe adui yangu! Nikianguka, nitainuka tena; Nikiwa gizani, Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu. Kwa vile nimemkosea Mwenyezi-Mungu, sina budi kuvumilia ghadhabu yake, mpaka atakapotetea kisa changu na kunijalia haki yangu. Atanileta nje kwenye mwanga, nami nitaona akithibitisha haki. Hapo adui yangu ataona hayo naye atajaa aibu; maana aliniambia: “Wapi basi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako?” Mimi mwenyewe nitamwona adui akianguka; atakanyagwakanyagwa chini kama tope la njiani. Siku yaja ambapo kuta za mji wenu zitajengwa upya. Siku hiyo mipaka ya nchi yenu itapanuliwa. Siku hiyo ndugu zenu watawarudia, kutoka Ashuru na vijiji vya Misri, kutoka nchi ya Misri na eneo la Eufrate; kutoka sehemu za maji na sehemu za milima. Lakini nchi yote nyingine itakuwa jangwa, kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Ee Mungu, uwachunge watu wako kwa fimbo yako, uwachunge hao walio kundi lako mwenyewe ambao wanaishi peke yao katika msitu wamezungukwa na ardhi yenye rutuba. Uwachunge kama ulivyofanya pale awali katika malisho ya Bashani na Gileadi. Kama wakati ulipotutoa nchini Misri, utuoneshe tena maajabu yako. Nao watu wa mataifa watakapoona hayo, watajaa fedheha hata kama wana nguvu. Watashikwa na bumbuazi na kukosa cha kusema na kuwa kama viziwi. Watatambaa mavumbini kama nyoka; naam, kama viumbe watambaao. Watatoka katika ngome zao huku wanatetemeka na kujaa hofu. Watakugeukia wewe Mungu wetu kwa hofu, wataogopa kwa sababu yako. Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe? Wewe wasamehe dhambi za watu wako waliobaki, wala huyaangalii makosa yao. Hasira yako haidumu milele, ila wapendelea zaidi kutuonesha fadhili zako. Utatuhurumia tena, ee Mwenyezi-Mungu; utafutilia mbali dhambi zetu, utazitupa zote katika vilindi vya bahari. Utaonesha uaminifu wako na rehema zako kwa wazawa wa Abrahamu na wa Yakobo, kama ulivyowaahidi wazee wetu tangu zamani. Kauli ya Mungu juu ya Ninewi. Kitabu cha maono ya Nahumu wa Elkoshi. Mwenyezi-Mungu ni Mungu mwenye wivu, mlipiza kisasi; Mwenyezi-Mungu hulipiza kisasi na ni mwenye ghadhabu; Mwenyezi-Mungu hulipiza kisasi kwa adui zake, huwaka ghadhabu juu ya adui zake. Mwenyezi-Mungu hakasiriki upesi, lakini amejaa nguvu, Mwenyezi-Mungu kamwe hatawaachilia wenye hatia. Apitapo Mwenyezi-Mungu, huzuka kimbunga na dhoruba; mawingu ni vumbi litimuliwalo na nyayo zake. Huikaripia bahari na kuikausha, yeye huikausha mito yote. Mbuga za Bashani na mlima Karmeli hunyauka, maua ya Lebanoni hudhoofika. Milima hutetemeka mbele yake, navyo vilima huyeyuka; dunia hutetemeka mbele yake, ulimwengu na vyote vilivyomo. Nani awezaye kuikabili ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu? Nani awezaye kustahimili ukali wa hasira yake? Yeye huimwaga hasira yake iwakayo kama moto, hata miamba huipasua vipandevipande. Mwenyezi-Mungu ni mwema, yeye ni ngome ya usalama wakati wa taabu. Yeye huwalinda wote wanaokimbilia usalama kwake. Adui wakiivamia nchi kama mafuriko, yeye huwaangamiza; huwafuatia na kuwafukuza mpaka gizani. Mbona mnafanya mipango dhidi ya Mwenyezi-Mungu? Yeye atawakomesha na kuwaangamiza, wala mpinzani wake hataweza kuinuka tena. Watateketezwa kama kichaka cha miiba, kama vile nyasi zilizokauka. Kwako kumetoka aliyepanga maovu dhidi ya Mwenyezi-Mungu aliyefanya njama za ulaghai. Mwenyezi-Mungu awaambia hivi watu wake: “Ingawa Waashuru ni wengi na wenye nguvu, wao wataangushwa na kuangamizwa. Ingawa nimewatesa nyinyi watu wangu, sitawateseni tena zaidi. Sasa nitaivunja nira ya Ashuru shingoni mwenu, na minyororo waliyowafungia nitaikatakata.” Mwenyezi-Mungu ameamuru hivi kuhusu Ninewi: “Hutapata wazawa kulidumisha jina lako. Sanamu zako za kuchonga na za kusubu, nitazivunjavunja nyumbani mwa miungu yako. Mimi nitakuchimbia kaburi lako, maana wewe hufai kitu chochote.” Enyi watu wa Yuda tazameni: Anakuja kutoka mlimani mtu anayeleta habari njema, mjumbe ambaye anatangaza amani. Adhimisheni sikukuu zenu, enyi watu wa Yuda, timizeni nadhiri zenu, maana waovu hawatawavamia tena, kwani wameangamizwa kabisa. Mwangamizi amekuja kukushambulia ee Ninewi. Chunga ngome zako! Weka ulinzi barabarani! Jiweke tayari! Kusanya nguvu zako zote! Mwenyezi-Mungu anamrudishia Yakobo fahari yake, naam, anawapa tena Waisraeli fahari yao, ingawa wavamizi hawakuwaachia kitu, hata matawi yao ya mizabibu waliyakata. Ngao za mashujaa wake ni nyekundu, askari wake wamevaa mavazi mekundu sana. Magari yao ya farasi yanamulika kama miali ya moto, yamepangwa tayari kushambulia; farasi hawatulii kwa uchu wa kushambulia. Magari ya farasi yanatimua mbio barabarani, yanakwenda huko na huko uwanjani. Yanamulika kama miali ya moto! Yanakwenda kasi kama umeme. Sasa anawaita maofisa wake, nao wanajikwaa wanapomwendea; wanakwenda ukutani himahima kutayarisha kizuizi. Vizuizi vya mito vimefunguliwa, ikulu imejaa hofu. Mji uko wazi kabisa, watu wamechukuliwa mateka. Wanawake wake wanaomboleza, wanalia kama njiwa, na kujipigapiga vifuani. Ninewi ni kama bwawa lililobomoka, watu wake wanaukimbia ovyo. “Simameni! Simameni!” Sauti inaita, lakini hakuna anayerudi nyuma. “Chukueni nyara za fedha, chukueni nyara za dhahabu! Hazina yake haina mwisho! Kuna wingi wa kila kitu cha thamani!” Mji wa Ninewi ni maangamizi matupu na uharibifu! Watu wamekufa moyo, magoti yanagongana, nguvu zimewaishia, nyuso zimewaiva! Limekuwaje basi hilo pango la simba, hilo lililokuwa maficho ya wanasimba? Pamekuwaje hapo mahali pa simba, mahali pa wanasimba ambapo hakuna aliyeweza kuwashtua? Simba dume amewararulia watoto wake nyama ya kutosha, akawakamatia simba majike mawindo yao; ameyajaza mapango yake mawindo, na makao yake mapande ya nyama. Tazama, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nitapambana nawe: Nitayateketeza kwa moto magari yako ya farasi, nitawamaliza kwa upanga hao simba wako vijana, nyara ulizoteka nitazitokomeza kutoka nchini, na sauti ya wajumbe wako haitasikika tena. Ole wako mji wa mauaji! Umejaa udanganyifu mtupu na nyara tele, usiokoma kamwe kuteka nyara. Sikia! Mlio wa mjeledi, mrindimo wa magurudumu, vishindo vya farasi na ngurumo za magari! Wapandafarasi wanashambulia, panga na mikuki inametameta; waliouawa hawana idadi, maiti wengi sana; watu wanajikwaa juu ya maiti! Ninewi! Wewe umekuwa kama malaya. Umewashawishi watu, ewe binti wa uchawi, uliyeyafanya mataifa kuwa watumwa kwa umalaya wako, na watu wa mataifa kwa uchawi wako. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema nitapambana nawe; nitalipandisha vazi lako hadi kichwani, niyaache mataifa yauone uchi wako, tawala ziikodolee macho aibu yako. Nitakutupia uchafu, na kukutendea kwa dharau, na kukufanya uwe kioja kwa watu. Kisha wote watakaokuona watakukimbia wakisema, “Ninewi umeangamizwa, ni nani atakayeuombolezea? Nani atakayekufariji?” Je, wewe Ninewi, ni bora kuliko Thebesi, mji uliojengwa kando ya mto Nili? Thebesi ulizungukwa na maji, bahari ilikuwa boma lake, maji yalikuwa ukuta wake! Kushi ilikuwa nguvu yake; nayo Misri pia, tena bila kikomo; watu wa Puti na Libia waliusaidia! Hata hivyo, ulichukuliwa mateka, watu wake wakapelekwa uhamishoni. Hata watoto wake walipondwapondwa katika pembe ya kila barabara; watu wake mashuhuri walinadiwa, wakuu wake wote walifungwa minyororo. Ninewi, nawe pia utalewa; utamkimbia adui na kujaribu kujificha. Ngome zako zote ni za tini za mwanzo; zikitikiswa zinamwangukia mlaji kinywani. Tazama askari wako: Wao ni waoga kama wanawake. Milango ya nchi yako ni wazi mbele ya adui zako; moto umeyateketeza kabisa makomeo yake. Tekeni maji muwe tayari kuzingirwa; imarisheni ngome zenu. Pondeni udongo kwa kuukanyagakanyaga, tayarisheni tanuri ya kuchomea matofali! Lakini huko pia moto utawateketezeni, upanga utawakatilia mbali; utawamaliza kama nzige walavyo. Ongezekeni kama nzige, naam, ongezekeni kama panzi! Wafanyabiashara wako waliongezeka kuliko nyota; lakini sasa wametoweka kama panzi warukavyo. Wakuu wako ni kama panzi, maofisa wako kama kundi la nzige; wakati wa baridi wanakaa kwenye kuta, lakini jua lichomozapo, huruka, wala hakuna ajuaye walikokwenda. Ewe mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wamelala, waheshimiwa wako wamesinzia. Watu wako wametawanyika milimani, wala hakuna yeyote wa kuwakusanya. Hakuna wa kuyapa nafuu majeraha yako, vidonda vyako ni vya kifo. Wote wanaosikia habari zako wanashangilia. Maana ni nani aliyeuepa ukatili wako usio na kikomo? Kauli ya Mungu aliyoiona nabii Habakuki. “Ee Mwenyezi-Mungu, nitakulilia mpaka lini, nawe usinisikilize na kunisaidia? Kwa nini nalia: ‘Dhuluma’ nawe hutuokoi? Kwa nini wanifanya nishuhudie mabaya na taabu? Uharibifu na ukatili vinanizunguka, ugomvi na mashindano yanazuka. Hivyo sheria haina nguvu, wala haki haitekelezwi. Waovu wanawazunguka waadilifu, hivyo hukumu hutolewa ikiwa imepotoshwa.” Mungu akasema: “Yaangalie mataifa, uone! Utastaajabu na kushangaa. Maana ninatenda kitu ukiwa bado unaishi, kitu ambacho ungeambiwa hungesadiki. Maana ninawachochea Wakaldayo, taifa lile kali na lenye hamaki! Taifa lipitalo katika nchi yote, ili kunyakua makao ya watu wengine. Wao ni watu wa kuchukiza na kutisha; wao hujiamulia wenyewe nini haki na adhama. “Farasi wao ni wepesi kuliko chui; wakali kuliko mbwamwitu wenye njaa. Wapandafarasi wao wanatoka mbali, wanaruka kasi kama tai arukiavyo mawindo. “Wote wanakuja kufanya ukatili; kwa nyuso kakamavu wanasonga mbele, wanakusanya mateka wengi kama mchanga. Wanawadhihaki wafalme, na kuwadharau watawala. Kila ngome kwao ni mzaha, wanairundikia udongo na kuiteka. Kisha wanasonga mbele kama upepo, wafanya makosa na kuwa na hatia, maana, nguvu zao ndizo mungu wao!” “Je, wewe si ndiwe Mwenyezi-Mungu, tangu kale na kale? Wewe ndiwe Mungu wangu, Mtakatifu wangu, usiyekufa Ee Mwenyezi-Mungu, umewateua Wakaldayo watuhukumu; Ewe Mwamba, umewaimarisha ili watuadhibu! Wewe ni mtakatifu kabisa, huwezi kutazama uovu, huwezi kustahimili kamwe kuona mabaya. Mbona basi wawaona wafanya maovu na kunyamaza, kwa nini unanyamaza waovu wanapowamaliza wale watu walio waadilifu kuliko wao? “Umewafanya watu kama samaki baharini, kama viumbe vitambaavyo visivyo na kiongozi! Wakaldayo huwavua watu kwa ndoana, huwavutia nje kwa wavu wao, huwakusanya wote katika jarife lao, kisha hufurahi na kushangilia. Kwa hiyo, wanazitambikia nyavu zao, na kuzifukizia ubani; maana kwa hizo huweza kuishi kwa anasa, na kula chakula cha fahari. “Je, hawataacha kamwe kuvuta upinde wao? Je, wataendelea tu kuwanasa watu, na kuyaangamiza mataifa bila huruma? Mimi nitasimama mahali pa kuchungulia, na kukaa juu mnarani; nitakaa macho nione ataniambia nini, atajibu nini kuhusu lalamiko langu.” Kisha, Mwenyezi-Mungu akanijibu hivi: “Yaandike maono haya; yaandike wazi juu ya vibao, anayepitia hapo apate kuyasoma. Maono haya yanangoja wakati wa kufaa; ni maono ya ukweli juu ya mwisho. Kama yaonekana kuchelewa, uyasubiri; hakika yatafika, wala hayatachelewa. Andika: ‘Waangalie wenye kiburi, hao wataangamia; lakini waadilifu wataishi kwa kumwamini Mungu.’” Zaidi ya hayo, divai hupotosha; mtu mwenye kiburi hatadumu. Yuko tayari kuwameza wengine kama Kuzimu; kama vile kifo, hatosheki na kitu. Hujikusanyia mataifa yote, na watu wote kama mali yake. Kila mtu atamdhihaki mtu wa namna hiyo na kumtungia misemo ya dhihaka: “Ole wako unayejirundikia visivyo vyako, na kuchukua rehani mali za watu lakini hulipi! Utaendelea kufanya hivyo hadi lini? Siku moja wadeni wako watainuka ghafla, wale wanaokutetemesha wataamka. Ndipo utakuwa mateka wao. Wewe umeyapora mataifa mengi, lakini wote wanaosalimika watakupora wewe, kwa mauaji na dhuluma uliyoitendea dunia, naam, uliyoifanyia miji na wakazi wake wote. “Ole wako unayejitajirisha kwa hasara ya mwingine, ujengaye nyumba yako juu milimani ukidhani kuwa salama mbali na madhara. Lakini kwa mipango yako umeiaibisha jamaa yako. Kwa kuyaangamiza mataifa mengi, umeyaangamiza maisha yako mwenyewe. Ndiyo maana hata mawe yatalalamika ukutani, na boriti za nyumba zitayaunga mkono. “Ole wako unayejenga mji kwa mauaji unayesimika jiji kwa maovu! Mwenyezi-Mungu wa majeshi husababisha juhudi za watu zipotelee motoni, na mataifa yajishughulishe bure. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu utaenea pote duniani, kama vile maji yaeneavyo baharini. Ole wako unayewalewesha jirani zako, na kutia sumu katika divai yao ili upate kuwaona wamekaa uchi. Utajaa aibu badala ya heshima. Utakunywa wewe mwenyewe na kupepesuka! Mwenyezi-Mungu mwenyewe atakulevya, na aibu itaifunika heshima yako! Maovu uliyoitenda Lebanoni yatakuvamia wewe; uliwaua wanyama, wanyama nao watakutisha. Yote hayo yatakupata wewe, kwa mauaji na dhuluma uliyoitendea dunia, naam, uliyoifanyia miji na wakazi wake wote. “Chafaa nini kinyago alichotengeneza mtu? Sanamu ni madini yaliyoyeyushwa, ni kitu cha kueneza udanganyifu! Mtengeneza sanamu hutumaini alichotengeneza mwenyewe, kinyago ambacho hakiwezi hata kusema! Ole wake mtu aliambiaye gogo: ‘Amka!’ Au jiwe bubu ‘Inuka!’ Je, sanamu yaweza kumfundisha mtu? Tazama imepakwa dhahabu na fedha, lakini haina uhai wowote.” Lakini Mwenyezi-Mungu yumo katika hekalu lake takatifu; dunia yote na ikae kimya mbele yake. Sala ya nabii Habakuki: Ee Mwenyezi-Mungu, nimesikia juu ya fahari yako, juu ya matendo yako, nami naogopa. Uyafanye tena mambo hayo wakati wetu; uyafanye yajulikane wakati huu wetu. Ukasirikapo tafadhali ukumbuke huruma yako! Mungu amekuja kutoka Temani, Mungu mtakatifu kutoka mlima Parani. Utukufu wake umetanda pote mbinguni, nayo dunia imejaa sifa zake. Mng'ao wake ni kama wa jua; miali imetoka mkononi mwake ambamo nguvu yake yadhihirishwa. Maradhi yanatangulia mbele yake, nyuma yake yanafuata maafa. Akisimama dunia hutikisika; akiyatupia jicho mataifa, hayo hutetemeka. Milima ya milele inavunjwavunjwa, vilima vya kudumu vinadidimia; humo zimo njia zake za kale na kale. Niliwaona watu wa Kushani wakiteseka, na watu wa Midiani wakitetemeka. Ee Mwenyezi-Mungu, je, umeikasirikia mito? Je, umeyakasirikia maji ya bahari, hata ukaendesha farasi wako, na magari ya vita kupata ushindi? Uliuweka tayari uta wako, ukaweka mishale yako kwenye kamba. Uliipasua ardhi kwa mito. Milima ilikuona, ikanyauka; mafuriko ya maji yakapita humo. Vilindi vya bahari vilinguruma, na kurusha juu mawimbi yake. Jua na mwezi vilikaa kimya katika makazi yao, vilipoona miali ya mishale yako ikienda kasi, naam, vilipouona mkuki wako ukimetameta. Kwa ghadhabu ulipita juu ya nchi, uliyakanyaga mataifa kwa hasira yako. Ulitoka kwenda kuwaokoa watu wako, kumwokoa yule uliyemweka wakfu kwa mafuta. Ulimponda kiongozi wa jamii ya waovu, ukawaangamiza kabisa wafuasi wake. Amiri jeshi ulimchoma mishale yako, jeshi lilipokuja kama kimbunga kututawanya, wakijigamba kuwaangamiza maskini mafichoni mwao. Kwa farasi wako ulitembea juu ya bahari, bahari inayosukwasukwa na mawimbi. Nasikia hayo nami ninashtuka mwilini, midomo yangu inatetemeka kwa hofu; mifupa yangu inateguka, miguu yangu inatetemeka. Ninangojea kwa utulivu siku ile ya maafa, ambayo inawajia wale wanaotushambulia. Hata kama mitini isipochanua maua, wala mizabibu kuzaa zabibu; hata kama mizeituni isipozaa zeituni, na mashamba yasipotoa chakula; hata kama kondoo wakitoweka zizini, na mifugo kukosekana mazizini, mimi nitaendelea kumfurahia Mwenyezi-Mungu nitamshangilia Mungu anayeniokoa. Bwana, Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu, huiimarisha miguu yangu kama ya paa, huniwezesha kupita juu milimani. Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amenia, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa mfalme Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda: Mwenyezi-Mungu asema: “Nitavifagilia mbali viumbe vyote duniani: Wanadamu, wanyama, ndege wa angani na samaki wa baharini; vyote nitaviangamiza. Waovu nitawaangamiza kabisa; wanadamu nitawafagilia mbali duniani. Nitaunyosha mkono wangu dhidi ya nchi ya Yuda, kadhalika na wakazi wote wa mji wa Yerusalemu. Nitaangamiza mabaki yote ya Baali kutoka nchi hii, na hakuna atakayetambua jina lao. Nitawaangamiza wote wanaosujudu juu ya paa, wakiabudu jeshi la mbinguni. Nitawaangamiza wale wanaoniabudu na kuapa kwa jina langu, hali wanaapa pia kwa jina la mungu Milkomu. Nitawaangamiza wote walioniacha mimi Mwenyezi-Mungu wote walioacha kunitafuta na kuniuliza shauri.” Nyamazeni mbele ya Bwana Mwenyezi-Mungu, kwani siku ya Mwenyezi-Mungu iko karibu. Mwenyezi-Mungu ameandaa tambiko, nao aliowaalika amewateua. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Katika siku ile ya karamu yangu, nitawaadhibu viongozi wa watu hao, kadhalika na wana wa mfalme pamoja na wote wanaoiga desturi za kigeni. Siku hiyo nitawaadhibu wote: Wanaoruka kizingiti cha nyumba kama wapagani, wanaojaza nyumba ya bwana wao vitu vya dhuluma na wizi. “Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, Kutasikika kilio kutoka Lango la Samaki, maombolezo kutoka Mtaa wa Pili, na mlio mkubwa kutoka milimani. Lieni enyi wakazi wa Makteshi! Wafanyabiashara wote wameangamia, wote wapimao fedha wamefutiliwa mbali. Wakati huo nitaupekua mji wa Yerusalemu kwa taa, nitawaadhibu wanaoishi wametulia kama machicha ya divai, wote ambao husema mioyoni mwao: ‘Mwenyezi-Mungu hatafanya kitu: Chema au kibaya.’ Utajiri wao utanyakuliwa, na nyumba zao zitaachwa tupu! Watajijengea nyumba, lakini hawataishi humo. Watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake.” Ile siku kubwa ya Mwenyezi-Mungu imekaribia, iko karibu na inakuja mbio. Mlio wa siku ya Mwenyezi-Mungu ni wa uchungu; hapo, shujaa atalia kwa sauti. Siku hiyo itakuwa siku ya ghadhabu, ni siku ya dhiki na uchungu, siku ya giza na huzuni; siku ya uharibifu na maangamizi, siku ya mawingu na giza nene. Siku hiyo ni ya mlio wa tarumbeta ya vita, dhidi ya miji yenye ngome na kuta ndefu. Kwa kuwa watu wamemkosea Mwenyezi-Mungu, yeye atawaletea dhiki kubwa, hivyo kwamba watatembea kama vipofu. Damu yao itamwagwa kama vumbi, na miili yao kama mavi. Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Kwa moto wa wivu wake dunia yote itateketezwa. Kwa ukamilifu na kwa namna ya kutisha atawafanya wakazi wote duniani watoweke. Kusanyikeni, kusanyikeni enyi taifa la watu wasio na aibu, kabla hamjapeperushwa mbali kama makapi, kabla haijawajia siku ya hasira kali ya Mwenyezi-Mungu, kabla haijawajia siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Mtafuteni Mwenyezi-Mungu enyi wanyenyekevu wote nchini, enyi mnaozitii amri zake. Tafuteni uadilifu, tafuteni unyenyekevu; labda mtaiepa siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Mji wa Gaza utahamwa, Ashkeloni utakuwa tupu. Wakazi wa Ashdodi watatimuliwa mchana, na wale wa Ekroni watang'olewa. Ole wenu wakazi wa nchi za pwani, watu mnaoishi huko Krete! Mwenyezi-Mungu ametamka dhidi yenu enyi wakazi wa Kanaani, nchi ya Filistia: Mimi nitawaangamiza asibaki hata mkazi mmoja! Nanyi nchi za pwani mtafanywa kuwa malisho; mtakuwa vibanda vya wachungaji na mazizi ya kondoo. Nchi ya pwani itamilikiwa na mabaki ya ukoo wa Yuda. Watachunga mifugo yao huko. Nyumba za mji wa Ashkeloni zitakuwa mahali pao pa kulala. Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wao atawakumbuka na kuwarudishia hali yao njema. “Nimeyasikia masuto ya Moabu na dhihaka za Waamoni; jinsi walivyowasuta watu wangu, na kujigamba kuiteka nchi yao. Kwa hiyo, niishivyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, mimi Mungu wa Israeli, Moabu itakuwa kama Sodoma na Amoni itakuwa kama Gomora. Nchi zake zitakuwa za viwavi na mashimo ya chumvi, zitakuwa ukiwa milele. Watu wangu watakaobaki wataziteka nyara, watu wa taifa langu waliosalia watazimiliki.” Hayo yatakuwa malipo ya kiburi chao, kwa sababu waliwadhihaki na kujigamba dhidi ya watu wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mwenyezi-Mungu atakuwa wa kutisha dhidi yao; miungu yote ya dunia ataikondesha. Mataifa yote duniani yatamsujudia; kila taifa katika mahali pake. Nanyi watu wa Kushi pia mtauawa kwa upanga wake. Mwenyezi-Mungu atanyosha mkono wake kaskazini, na kuiangamiza nchi ya Ashuru. Ataufanya mji wa Ninewi kuwa ukiwa, kuwa mahali pakavu kama jangwa. Makundi ya mifugo yatalala humo, kadhalika kila mnyama wa porini. Tai na yangeyange na korongo wataishi juu ya nguzo zake, bundi watalia kwenye madirisha yake, kunguru watalia kwenye vizingiti, maana nyumba zake za mierezi zitakuwa tupu. Je, huu ndio mji uliojivuna na kuishi kwa usalama, mji uliojisemea, “Ni mimi tu, hakuna mwingine!” Jinsi gani umekuwa mtupu na makao ya wanyama wa mwituni! Kila apitaye karibu atauzomea na kuudharau. Ole wake mji wa Yerusalemu, mji mchafu, najisi na mdhalimu. Hausikilizi onyo lolote, wala haukubali kukosolewa. Haukumtegemea Mwenyezi-Mungu kamwe, wala kumkaribia Mungu wake. Viongozi wake ni simba wangurumao, mahakimu wake ni mbwamwitu wenye njaa jioni wasioacha chochote mpaka asubuhi. Manabii wake ni watu wasiojali na wadanganyifu. Makuhani wake wamevitia unajisi vitu vitakatifu na kuihalifu sheria kwa nguvu. Lakini Mwenyezi-Mungu aliye mjini humo ni mwadilifu, yeye hatendi jambo lolote baya. Kila siku asubuhi hudhihirisha kauli yake, naam, kila kunapopambazuka huitekeleza. Lakini wahalifu hawana aibu hata kidogo. Mwenyezi-Mungu asema: “Nimeyafutilia mbali mataifa; kuta zao za kujikinga ni magofu. Barabara zao nimeziharibu, na hamna apitaye humo. Miji yao imekuwa mitupu, bila watu, na bila wakazi. Nilisema, ‘Hakika mji huu watanicha na kukubali kukosolewa; hautaacha kukumbuka mara hizo zote nilizowaadhibu.’ Lakini watu wake walizidisha tamaa zao za kufanya matendo yao kuwa upotovu. “Kwa hiyo ningojeni mimi Mwenyezi-Mungu, ngoja siku nitakapoinuka kutoa mashtaka. Nimeamua kuyakusanya mataifa na falme, kuyamwagia ghadhabu yangu, kadhalika na ukali wa hasira yangu. Dunia yote itateketezwa kwa moto wa ghadhabu yangu. “Wakati huo nitaibadili lugha ya watu, nitawawezesha kusema lugha adili ili waniite mimi Mwenyezi-Mungu, na kuniabudu kwa moyo mmoja. Kutoka ng'ambo ya mito ya Kushi watu wangu wanaoniomba ambao wametawanyika, wataniletea sadaka yangu. “Siku hiyo, haitakulazimu kuona aibu, kutokana na matendo yako ya kuniasi, maana nitawaondoa miongoni mwako wale wanaojigamba na kujitukuza nawe hutakuwa na kiburi tena katika mlima wangu mtakatifu. Nitakuachia watu wapole na wanyenyekevu ambao watakimbilia usalama kwangu mimi Mwenyezi-Mungu. Waisraeli watakaobaki, hawatatenda mabaya wala hawatasema uongo; wala kwao hatapatikana mdanganyifu yeyote. Watapata malisho na kulala wala hakuna mtu atakayewatisha.” Imba kwa sauti, ewe Siyoni, paza sauti ee Israeli. Furahi na kushangilia kwa moyo wote, ewe Yerusalemu! Mwenyezi-Mungu amekuondolea hukumu iliyokukabili, amewageuzia mbali adui zako. Mwenyezi-Mungu, mfalme wa Israeli yuko pamoja nawe hutaogopa tena maafa. Siku hiyo, mji wa Yerusalemu utaambiwa: “Usiogope, ee Siyoni, usilegee mikono. Mwenyezi-Mungu, Mungu wako yu pamoja nawe yeye ni shujaa anayekuletea ushindi. Yeye atakufurahia kwa furaha kuu, kwa upendo wake atakujalia uhai mpya. Atakufurahia kwa wimbo wa sauti kubwa, kama vile katika siku ya sikukuu.” Mwenyezi-Mungu asema: “Nitakuondolea maafa yako, nawe hutahitaji kuona aibu kwa ajili yake. Wakati huo, nitawaadhibu wote wanaokukandamiza. Nitawaokoa vilema na kuwakusanya waliotupwa, na kubadili aibu yao kuwa sifa na fahari duniani kote. Wakati huo nitawakusanya, na kuwafanya mjulikane na kusifiwa, miongoni mwa watu wote duniani nitakapowarudishia hali yenu njema nanyi muone kwa macho yenu wenyewe. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Siku ya kwanza ya mwezi wa sita mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario wa Persia, Mwenyezi-Mungu alimpa Hagai ujumbe aupeleke kwa Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mkuu wa Yuda, na kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Hagai akasema: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: Watu hawa wanasema kwamba wakati wa kulijenga upya hekalu langu haujafika.” Lakini Mwenyezi-Mungu ameniambia mimi nabii Hagai, “Je, ni sawa kwenu kukaa katika majumba yenu ya fahari hali hekalu langu ni magofu matupu?” Sasa, asema hivi Mwenyezi-Mungu: “Fikirini kama mnafanya sawa! Nyinyi mmepanda mbegu kwa wingi, lakini mmevuna kidogo; mnakula, lakini hamshibi; mnakunywa divai, lakini hamtosheki; mnavaa nguo, lakini bado mnasikia baridi; mfanyakazi mshahara wake huwa kama umetumbukizwa katika mfuko uliotoboka.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Fikirini kama mnafanya sawa! Sasa, basi, nendeni milimani mkalete miti, mlijenge upya hilo hekalu, nipate kulifurahia na kutukuzwa. “Mlitazamia mavuno mengi, lakini mlipata kidogo tu. Na mlipoyaleta nyumbani, niliyapeperusha mbali. Kwa nini? Kwa sababu hekalu langu ni magofu matupu hali kila mmoja wenu anashughulikia nyumba yake. Ndio maana mbingu zimeacha kunyesha mvua, nayo ardhi haioteshi mavuno. Nimeleta ukame nchini, ukaathiri vilima na mashamba ya nafaka, mashamba ya mizabibu na mashamba ya mizeituni na kila mmea, watu na wanyama, na chochote mlichotolea jasho.” Ndipo Zerubabeli mwana wa Shealtieli, na kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, pamoja na watu wote waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni wakafanya kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wao alivyowaambia na kama walivyoambiwa na nabii Hagai, kama alivyotumwa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Watu wakamcha Mwenyezi-Mungu. Kisha Hagai, mjumbe wa Mwenyezi-Mungu, akawapa watu ujumbe ufuatao kutoka kwa Mwenyezi-Mungu: Mwenyezi-Mungu asema: “Mimi nipo pamoja nanyi.” Basi, Mwenyezi-Mungu akawapa moyo Zerubabeli mkuu wa Yuda, kuhani mkuu Yoshua na watu wote waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni, walishughulikie hekalu. Walianza kazi hiyo ya kulijenga upya hekalu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao, mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa sita, mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario. Mnamo siku ya ishirini na moja, mwezi wa saba mwaka huohuo, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia nabii Hagai. Alimwambia Hagai aongee na mkuu wa Yuda, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki na watu wote waliorudi kutoka uhamishoni awaambie hivi: “Je, kuna yeyote kati yenu asiyekumbuka jinsi hekalu hili lilivyokuwa la fahari? Sasa mnalionaje? Bila shaka sasa mnaliona kama si kitu! Hata hivyo, usife moyo, ewe Zerubabeli. Jipe moyo, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Jipeni moyo nanyi watu wote wa nchi hii. Fanyeni kazi, maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nipo pamoja nanyi. Mlipotoka Misri niliwaahidi kwamba daima nitakuwa pamoja nanyi. Basi, ningali pamoja nanyi, kwa hiyo, msiogope kitu. “Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema, hivi karibuni nitazitikisa mbingu na dunia, bahari na nchi kavu. Nitayatikisa mataifa yote na hazina zao zote zitaletwa humu, nami nitalifanya hekalu hili kuwa la fahari. Mimi nimesema. Fedha na dhahabu yote duniani ni mali yangu. Hekalu jipya litakuwa lenye fahari zaidi kuliko lile la awali, na mahali hapo ndipo nitakapowapa watu wangu fanaka.” Asema Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi lilimjia nabii Hagai, akamwambia: “Waambie makuhani watoe uamuzi juu ya jambo hili: Kama mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa vazi lake, kisha akagusa kwa upindo wa vazi hilo mkate au chakula kilichopikwa, au divai, au mafuta au chakula cha aina yoyote ile, je, chakula hicho kitakuwa kitakatifu?” Makuhani wakamjibu, “La, hasha.” Hagai akawauliza tena, “Je, mtu aliye najisi kwa kugusa maiti, akigusa baadhi ya vyakula hivi, chakula hicho kitakuwa najisi?” Makuhani wakamjibu, “Ndiyo, kitakuwa najisi.” Hapo Hagai akawaambia, “Mwenyezi-Mungu asema kwamba, hivyo ndivyo ilivyo kwa watu wa taifa hili na kila kitu wanachofanya; kadhalika na kila wanachotoa madhabahuni ni najisi. “Lakini sasa angalieni mambo yatakayotukia. Kabla ya kuanza kujenga upya hekalu langu, hali yenu ilikuwaje? Mliliendea fungu la nafaka mkitarajia kupata vipimo ishirini, lakini kulikuwa na vipimo kumi tu. Mliliendea pipa la divai mkitarajia kujaza vyombo hamsini, lakini mlikuta ishirini tu. Niliwapiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, nikaharibu kila mlichojaribu kupanda, lakini hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Leo ni siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, siku ambayo msingi wa hekalu umekamilika. Basi, ngojeni mwone yale yatakayotokea tangu leo. Ingawa sasa hamna nafaka ghalani, nayo mizabibu, mitini, mikomamanga na mizeituni haijazaa kitu, lakini tangu leo, nitawabariki.” Siku hiyohiyo ya ishirini na nne, mwezi wa tisa, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Hagai mara ya pili: “Ongea na Zerubabeli mkuu wa Yuda, umwambie hivi: Niko karibu kuzitikisa mbingu na dunia, kuangusha falme na kukomesha nguvu zao. Nitayapindua magari yao ya farasi na wapandafarasi wake, nao wataanguka na kuuana wao kwa wao. Siku hiyo, nitakuchukua wewe mtumishi wangu Zerubabeli mwana wa Shealtieli, na kukuteua ili utawale kwa jina langu. Wewe ndiwe niliyekuchagua.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amesema. Mnamo mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario wa Persia, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido: “Mimi Mwenyezi-Mungu nilichukizwa sana na wazee wenu. Basi, waambie watu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Nirudieni, nami nitawarudieni nyinyi. Msiwe kama wazee wenu ambao manabii waliwaambia waachane na mienendo yao miovu na matendo yao mabaya, lakini wao hawakunisikiliza wala hawakunitii mimi Mwenyezi-Mungu. Wazee wenu, wako wapi? Na manabii, je, wanaishi milele? Je, wazee wenu hawakupata adhabu kwa sababu ya kukataa maagizo yangu na amri nilizowapa kwa njia ya watumishi wangu manabii? Wakati huo, wao walitubu na kusema kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nilikusudia kuwatenda kulingana na mienendo yao na matendo yao, na kweli ndivyo nilivyowatenda.” Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi wa Shebati, mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia mimi nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido, kama ifuatavyo: Wakati wa usiku, nilimwona malaika amepanda farasi mwekundu. Malaika huyo alikuwa amesimama bondeni, katikati ya miti ya mihadasi. Nyuma yake kulikuwa na farasi wengine wekundu, wa kijivujivu na weupe. Basi, nikamwuliza, “Bwana, Farasi hawa wanamaanisha nini?” Malaika huyo aliyeongea nami akaniambia, “Nitakuonesha hao farasi wanamaanisha nini. Hawa ndio waliotumwa na Mwenyezi-Mungu kuikagua dunia.” Hao farasi wakamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumeikagua dunia yote, nayo kweli imetulia.” Ndipo huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kwa muda gani utaendelea kutokuwa na huruma juu ya mji wa Yerusalemu na miji ya nchi ya Yuda ambayo umeikasirikia kwa muda wa miaka sabini?” Mwenyezi-Mungu akampa huyo malaika jibu jema na lenye matumaini. Basi, huyo malaika akaniambia, “Unapaswa kutangaza kwa sauti kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Moyo wangu umejaa upendo kwa mji wa Yerusalemu, naam, kwa mlima Siyoni. Walakini nimechukizwa sana na mataifa ambayo yanastarehe. Kweli niliwakasirikia Waisraeli kidogo, lakini mataifa hayo yaliwaongezea maafa. Kwa hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, naurudia mji wa Yerusalemu kwa huruma; humo itajengwa nyumba yangu, na ujenzi mpya wa mji utaanza.’” Kisha malaika huyo akaniambia nitangaze ujumbe huu mwingine: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Miji yangu itafurika tena fanaka. Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji tena mji wa Siyoni; nitauteua mji wa Yerusalemu kuwa wangu.’” Katika maono mengine, niliona pembe nne. Nami nikamwuliza yule malaika aliyezungumza nami, “Pembe hizi zinamaanisha nini?” Yeye akanijibu, “Pembe hizi zinamaanisha yale mataifa ambayo yaliwatawanya watu wa Yuda, Israeli na Yerusalemu.” Kisha, Mwenyezi-Mungu akanionesha wafuachuma wanne. Nami nikauliza, “Watu hawa wanakuja kufanya nini?” Yeye akanijibu, “Watu hawa wamekuja kuyatisha na kuyaangamiza yale mataifa yenye nguvu ambayo yaliishambulia nchi ya Yuda na kuwatawanya watu wake.” Katika maono mengine, nilimwona mtu aliyekuwa na kamba ya kupimia mkononi mwake. Basi, nikamwuliza, “Unakwenda wapi?” Naye akanijibu, “Ninakwenda kuupima urefu na upana wa mji wa Yerusalemu.” Yule malaika aliyezungumza nami akawa anamwendea malaika mwingine ambaye alikuwa anamjia. Basi, huyo malaika aliyezungumza nami akamwambia huyo mwenzake, “Kimbia ukamwambie yule kijana kwamba si lazima mji wa Yerusalemu uwe na kuta, la sivyo hapatakuwa na nafasi ya kuwatosha wakazi wake wengi na mifugo itakayokuwa ndani yake. Mwenyezi-Mungu asema kuwa yeye mwenyewe atakuwa ukuta wa moto kuulinda mji huo pande zote, naye atakaa humo kwa utukufu wake.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Haya! Kimbieni kutoka nchi ya kaskazini ambako mimi nilikuwa nimewatawanya kila upande. Haraka! Nyinyi nyote mnaokaa katika nchi ya Babuloni, kimbilieni huko mjini Siyoni!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ambaye kwa utukufu wake amenituma, asema hivi juu ya mataifa yaliyowateka nyara watu wake: “Hakika, anayewagusa nyinyi anagusa mboni ya jicho langu. Naam, nitachukua hatua dhidi ya hao waliowatekeni nyara, nao watatekwa nyara na wale waliowafanya watumwa wao.” Hapo ndipo mtakapojua kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndiye aliyenituma. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wa Siyoni, imbeni na kufurahi kwa kuwa ninakuja na kukaa kati yenu. Mataifa mengi yatajiunga nami Mwenyezi-Mungu, nao watakuwa watu wangu; nami nitakaa kati yenu.” Mambo hayo yatakapotukia ndipo mtakapojua kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndiye aliyenituma kwenu. Watu wa Yuda watakuwa tena mali ya pekee ya Mwenyezi-Mungu katika nchi takatifu, na mji wa Yerusalemu utakuwa tena mji wake aliouchagua. Enyi wanadamu wote, nyamazeni mbele ya Mwenyezi-Mungu, maana, yeye anakuja kutoka makao yake matakatifu. Katika maono mengine, Mwenyezi-Mungu alinionesha kuhani mkuu Yoshua amesimama mbele ya malaika wa Mwenyezi-Mungu, na upande wake wa kulia amesimama Shetani kumshtaki. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia huyo Shetani, “Mwenyezi-Mungu na akulaani, ewe Shetani! Naam, Mwenyezi-Mungu aliyeuteua mji wa Yerusalemu na akulaani! Mtu huyu ni kama kinga kilichonyakuliwa kutoka motoni!” Kuhani mkuu Yoshua alikuwa amesimama mbele ya malaika, akiwa amevaa mavazi machafu. Malaika akawaambia watumishi wake, “Mvueni kuhani mkuu Yoshua mavazi yake machafu.” Kisha akamwambia kuhani mkuu Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakupa mavazi ya thamani.” Kisha akawaambia wamvike kilemba safi kichwani. Hivyo, wakamvika kilemba safi na mavazi; naye malaika wa Mwenyezi-Mungu alikuwa amesimama hapo. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwonya kuhani mkuu Yoshua, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Ukifuata mwongozo wangu na kuyazingatia maagizo niliyokupa, basi, utaisimamia nyumba yangu na nyua zake. Nami nitakuwezesha kuingia katika utumishi wangu kama hawa wanaosimama mbele yangu. Sasa sikiliza kwa makini, ewe Yoshua, kuhani mkuu; sikilizeni pia enyi makuhani wenzake mlio pamoja naye, nyinyi mlio ishara ya wakati mzuri ujao: Nitamleta mtumishi wangu aitwaye Tawi. Kumbukeni kuwa nimeweka mbele ya Yoshua jiwe moja lenye nyuso saba. Nami nitachora maandishi juu yake, na kwa siku moja tu, nitaiondoa dhambi ya nchi hii. Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Siku hiyo, kila mmoja wenu atamwalika mwenzake kufurahia amani na utulivu katika shamba lake la mizabibu na la mitini.’” Yule malaika aliyeongea nami, akanijia tena, akaniamsha kama kumwamsha mtu usingizini. Akaniuliza, “Unaona nini?” Nami nikamjibu, “Ninaona kinara cha taa cha dhahabu. Juu yake kuna bakuli la mafuta na taa saba, na kila moja ina mahali pa kutilia tambi saba. Karibu na kinara hicho kuna miti miwili ya mzeituni; mmoja upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto.” Basi, nikamwuliza huyo malaika, “Bwana, vitu hivi vinamaanisha nini?” Naye akanijibu, “Hujui vitu hivi vinamaanisha nini?” Nikamjibu, “Sijui bwana.” *** *** *** *** Huyo malaika akaniambia, “Hizo taa saba ni macho saba ya Mwenyezi-Mungu yaonayo kila mahali duniani.” Nami nikazidi kuuliza, “Je, hiyo miti miwili ya mizeituni iliyo upande wa kulia na wa kushoto wa kinara, inamaanisha nini? Na hayo matawi mawili pembeni mwa mirija miwili ya dhahabu ambamo mafuta ya mizeituni hutiririkia, yanamaanisha nini?” Naye akaniambia, “Je, hujui?” Nami nikamjibu, “La, sijui Bwana!” Hapo akaniambia, “Matawi haya ndio wale watu wawili waliowekwa wakfu kwa mafuta wamtumikie Bwana wa ulimwengu wote.” Ahadi ya Mungu kwa Zerubabeli Naye akaniambia pia niseme neno hili la Mwenyezi-Mungu kumhusu Zerubabeli: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: Huwezi kushinda kwa nguvu au kwa uwezo wako mwenyewe, bali kwa msaada wa roho yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema.” Tena, akaongeza kusema: “Je, mlima huu ni kizuizi? La! Wewe Zerubabeli utausawazisha. Wewe utaanzisha ujenzi mpya wa hekalu, na wakati utakapoliweka jiwe la mwisho, watu watashangilia wakisema, ‘Ni zuri! Naam, ni zuri!’” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Zerubabeli ameuweka msingi wa hekalu naye pia atalikamilisha. Hayo yatakapotukia, watu wangu watajua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndimi niliyekutuma kwao. Maendeleo ya ujenzi wa hekalu yanaonekana madogo, na watu wanayadharau; lakini watamwona Zerubabeli akiendelea kulijenga hekalu, nao watafurahi.” Nilipotazama tena niliona kitabu kinaruka angani. Yule malaika akaniuliza, “Unaona nini?” Nami nikamjibu, “Ninaona kitabu kinaruka angani; urefu wake ni mita tisa na upana wake ni mita nne na nusu.” Basi, yeye akaniambia, “Ndani ya kitabu hicho kumeandikwa laana ambayo itaikumba nchi nzima. Upande mmoja imeandikwa kwamba wezi wote watafukuzwa nchini, na upande mwingine imeandikwa kwamba wote wenye kuapa uongo kadhalika watafanyiwa vivyo hivyo. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema kuwa yeye mwenyewe ataipeleka laana hiyo. Itapenya kila nyumba ya mwizi na kila nyumba ya mwenye kuapa uongo kwa kutumia jina lake; itakaa humo na kuteketeza nyumba hiyo yote, mbao na mawe.” Yule malaika aliyeongea nami alinikaribia, akaniambia, “Hebu tazama uone kile kinachokuja.” Nami nikamwuliza, “Ni kitu gani hicho?” Naye akanijibu, “Hicho ni kikapu chenye makosa ya nchi nzima.” Kikapu chenyewe kilikuwa na mfuniko uliotengenezwa kwa risasi; kilifunuliwa, nami nikaona mwanamke ameketi humo ndani. Yule malaika akaniambia, “Mwanamke huyo anawakilisha uovu!” Kisha huyo malaika akamsukumia ndani ya kikapu mwanamke huyo na kukifunika. Nilipotazama juu, niliona wanawake wawili wanatokea kunijia; walikuwa wakirushwa na upepo, nao walikuwa na mabawa yenye nguvu kama ya korongo. Wanawake hao wakakiinua kile kikapu angani. Basi, nikamwuliza yule malaika aliyezungumza nami, “Wanakipeleka wapi kile kikapu?” Naye akaniambia “Wanakipeleka katika nchi ya Shinari. Huko watakijengea hekalu na litakapokuwa tayari, watakiweka kikapu hicho ndani.” Niliona maono mengine tena. Safari hii, niliona magari manne ya farasi yakitoka katikati ya milima miwili ya shaba nyeusi. Gari la kwanza lilikokotwa na farasi wekundu, la pili lilikokotwa na farasi weusi, la tatu lilikokotwa na farasi weupe, na la nne lilikokotwa na farasi wa kijivujivu. Basi, nikamwuliza yule malaika aliyeongea nami, “Bwana, magari haya ya farasi yanamaanisha nini?” Malaika akanijibu, “Magari haya ni pepo kutoka pande nne za mbingu. Yalikuwa mbele ya Mwenyezi-Mungu wa dunia nzima, na sasa yanaondoka. Lile gari linalokokotwa na farasi weusi linakwenda kaskazini, lile linalokokotwa na farasi weupe linakwenda magharibi, na lile linalokokotwa na farasi wa kijivujivu linakwenda kusini.” Farasi hao walipotokea walikuwa na hamu sana ya kwenda kuikagua dunia. Naye malaika akawaambia, “Haya! Nendeni mkaikague dunia.” Basi, wakaenda na kuikagua dunia. Kisha yule malaika aliyeongea nami akaniambia kwa sauti, “Tazama! Wale farasi waliokwenda nchi ya kaskazini wameituliza ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Pokea zawadi za watu walio uhamishoni zilizoletwa na Heldai, Tobia na Yedaya. Nenda leo hii nyumbani kwa Yosia, mwana wa Sefania ambamo watu hao wamekwenda baada ya kuwasili kutoka Babuloni. Utachukua fedha na dhahabu hiyo, utengeneze taji ambalo utamvika kuhani mkuu Yoshua, mwana wa Yehosadaki, na kumwambia kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Hapa pana mtu aitwaye Tawi. Yeye atastawi hapo alipo na kulijenga hekalu langu mimi Mwenyezi-Mungu. Yeye ndiye atakayelijenga hekalu langu mimi Mwenyezi-Mungu Atapewa heshima ya kifalme na kuketi kwenye kiti chake cha enzi kuwatawala watu wake. Karibu na kiti cha enzi cha mtawala huyo, atakaa kuhani mkuu, nao wawili watafanya kazi pamoja kwa amani. Taji hilo itahifadhiwa katika hekalu langu kwa heshima ya Heldai, Tobia, Yedaya na Yosia mwana wa Sefania.’ “Watu wanaokaa nchi za mbali watakuja kusaidia kulijenga hekalu langu mimi Mwenyezi-Mungu.” Nanyi mtajua kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndiye aliyenituma kwenu. Haya yote yatatukia kama mkiitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mnamo mwaka wa nne wa utawala wa mfalme Dario, siku ya nne ya mwezi wa tisa, yaani Kislevu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia mimi Zekaria. Watu wa mji wa Betheli walikuwa wamewatuma Sharesa na Regem-meleki pamoja na watu wao kumwomba Mwenyezi-Mungu fadhili zake, na kuwauliza makuhani wa hekalu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi na manabii swali hili: “Je, tuendelee kuomboleza na kufunga katika mwezi wa tano kama tulivyofanya kwa muda wa miaka mingi sasa?” Hapo, neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi likanijia: “Waambie wakazi wote wa nchi na makuhani hivi: ‘Kwa muda wa miaka sabini iliyopita, nyinyi mmekuwa mkifunga na kuomboleza mnamo mwezi wa tano na wa saba. Je, mnadhani mlifunga kwa ajili yangu? Je, mnapokula na kunywa, si mnakula na kunywa kwa ajili yenu wenyewe?’ Haya ndiyo mambo ambayo mimi Mwenyezi-Mungu niliwaambieni kupitia kwa manabii wa hapo kwanza, wakati mji wa Yerusalemu ulikuwa umestawi na wenye wakazi tele, na wakati ambapo kulikuwa na wakazi wengi katika miji ya kandokando yake na katika eneo la Negebu na nyanda za Shefela.” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mimi Zekaria: “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Amueni kwa haki, muwe na upole na huruma nyinyi kwa nyinyi. Msiwadhulumu wajane, yatima, wageni au maskini; msikusudie mabaya mioyoni mwenu dhidi yenu wenyewe. “Lakini watu walikataa kunisikiliza, wakakaidi na kuziba masikio yao ili wasisikie. Wakaifanya mioyo yao kuwa migumu kama jiwe, wasije wakasikia sheria yangu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi niliyoitangaza kwa roho yangu kwa kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nikawaka hasira dhidi yao, nikasema, ‘Kwa kuwa niliwaita nao hawakunisikiliza, basi, nao waliponiita, sikuwasikiliza. Nami niliwatawanya kwa kimbunga kati ya mataifa yote ambayo hawakuyajua. Hivyo nchi waliyoiacha ikabaki tupu; hapakuwa na mtu yeyote aliyekaa humo; naam, nchi hiyo ya kupendeza ikawa ukiwa.’” Neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi likanijia mimi Zekaria: “Ninawaka upendo mkuu kwa ajili ya Siyoni, na ninawaka ghadhabu nyingi dhidi ya adui zake. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema hayo. Nitaurudia mji wa Siyoni na kufanya makao yangu mjini Yerusalemu. Mji wa Yerusalemu utaitwa ‘Mji Mwaminifu,’ na mlima wangu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, utaitwa ‘Mlima Mtakatifu.’ Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Wazee, wanaume kwa wanawake, wataonekana tena wamekaa kwenye barabara za Yerusalemu, kila mmoja na mkongojo wake kwa sababu ya kuishi miaka mingi. Barabara za Yerusalemu zitajaa wavulana na wasichana, wakichezacheza humo. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Kwa watu hawa waliosalia, hali hii inaonekana kuwa kitu kisichowezekana; lakini mnadhani haiwezekani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi? Nitawaokoa watu wangu kutoka nchi ya mashariki na kutoka nchi ya magharibi na kuwafanya wakae katika mji wa Yerusalemu. Wao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao; nitatawala juu yao kwa uaminifu na haki.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Jipeni moyo! Sasa mnayasikia maneno ambayo mlitangaziwa na manabii wakati ulipowekwa msingi wa hekalu langu, kulijenga upya. Kabla ya wakati huo, watu hawakupata mshahara kwa kazi zao wala kwa kukodisha mnyama. Hamkuwa na usalama kwa sababu ya adui zenu, maana nilisababisha uhasama kati ya watu wote. Lakini sasa sitawatendea hao watu wa taifa hili waliosalia kama hapo zamani. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Sasa nitaleta tena amani duniani, mvua itanyesha kama kawaida, ardhi itatoa mazao, na mizabibu itazaa kwa wingi. Nitawapa watu waliosalia wa taifa hili hayo yote yawe mali yao. Enyi watu wa Yuda na watu wa Israeli! Wakati uliopita nyinyi mlionekana kuwa watu waliolaaniwa kati ya watu wa mataifa. Lakini sasa mimi nitawaokoeni, nanyi mtakuwa watu waliobarikiwa. Basi, msiogope tena, bali jipeni moyo!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Kama nilivyokusudia kuwatendea nyinyi maovu kwa sababu wazee wenu walinikasirisha, na wala sikuwaonea huruma, vivyo hivyo nimekusudia kuutendea wema mji wa Yerusalemu na watu wa Yuda. Basi, msiogope. Hivi ndivyo mnavyopaswa kufanya: Kila mmoja wenu na amwambie mwenzake ukweli. Mahakama yenu daima na yatoe hukumu za haki ziletazo amani. Mtu yeyote miongoni mwenu asikusudie kutenda uovu dhidi ya mwenzake, wala msiape uongo, maana nayachukia sana matendo hayo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi lilinijia mimi Zekaria: “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Siku za mfungo za mwezi wa nne, mwezi wa tano, mwezi wa saba na mwezi wa kumi, zitakuwa nyakati za furaha na shangwe; zitakuwa sikukuu za sherehe kwa watu wa Yuda. Basi, pendeni ukweli na amani.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Watu wengi wa mataifa ya kigeni na wakazi wa miji mingi watamiminika mjini Yerusalemu. Wakazi wa mji mmoja watawaendea wakazi wa mji mwingine na kuwaambia, ‘Twendeni pamoja kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi na kumwomba baraka!’ Naam, mataifa yenye nguvu na watu wengi watakuja Yerusalemu kuniabudu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi na kuniomba baraka. Wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, watu kumi kutoka mataifa ya kila lugha watamng'ang'ania Myahudi mmoja na kushika nguo yake na kumwambia, ‘Tunataka kwenda pamoja nanyi, kwa sababu tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nanyi.’” Kauli ya Mwenyezi-Mungu: Mwenyezi-Mungu ametamka siyo tu dhidi ya nchi ya Hadraki bali pia dhidi ya Damasko. Maana nchi ya Aramu ni mali ya Mwenyezi-Mungu, kama vile yalivyo makabila yote ya Israeli. Hali kadhalika mji wa Hamathi unaopakana na Hadraki; na hata miji ya Tiro na Sidoni ingawaje yajiona kuwa na hekima sana. Mji wa Tiro umejijengea ngome kumbwa, umejirundikia fedha kama vumbi, na dhahabu kama takataka barabarani. Lakini Bwana ataichukua mali yake yote, utajiri wake atautumbukiza baharini, na kuuteketeza mji huo kwa moto. Mji wa Ashkeloni utaona hayo na kuogopa, nao mji wa Gaza utagaagaa kwa uchungu; hata Ekroni, maana tumaini lake litatoweka. Mji wa Gaza utapoteza mfalme wake, nao Ashkeloni hautakaliwa na watu. Mji wa Ashdodi utakaliwa na machotara. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kiburi cha Filistia nitakikomesha. Nitawakomesha kula nyama yenye damu, na chakula ambacho ni chukizo. Mabaki watakuwa mali yangu, kama ukoo mmoja katika Yuda. Watu wa Ekroni watakuwa kama Wayebusi. Mimi mwenyewe nitailinda nchi yangu, nitazuia majeshi yasipitepite humo. Hakuna mtu atakayewadhulumu tena watu wangu, maana, kwa macho yangu mwenyewe, nimeona jinsi walivyoteseka.” Shangilieni sana enyi watu wa Siyoni! Paazeni sauti, enyi watu wa Yerusalemu! Tazama, mfalme wenu anawajieni, anakuja kwa shangwe na ushindi! Ni mpole, amepanda punda, mwanapunda, mtoto wa punda. Atatokomeza magari ya vita nchini Efraimu, na farasi wa vita kutoka mjini Yerusalemu; pinde za vita zitavunjiliwa mbali. Naye ataleta amani miongoni mwa mataifa; utawala wake utaenea toka bahari hata bahari, toka mto Eufrate hata miisho ya dunia. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kwa sababu ya agano langu nanyi, agano lililothibitishwa kwa damu, nitawakomboa wafungwa wenu walio kama wamefungwa katika shimo tupu. Enyi wafungwa wenye tumaini; rudini kwenye ngome yenu. Sasa mimi ninawatangazieni: Nitawarudishieni mema maradufu. Yuda nitamtumia kama uta wangu; Efraimu nimemfanya mshale wangu. Ee Siyoni! Watu wako nitawatumia kama upanga kuwashambulia watu wa Ugiriki; watakuwa kama upanga wa shujaa.” Mwenyezi-Mungu atawatokea watu wake; atafyatua mishale yake kama umeme. Bwana Mwenyezi-Mungu atapiga tarumbeta; atafika pamoja na kimbunga cha kusini. Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawalinda watu wake, nao watawaangamiza maadui zao. Watapiga kelele vitani kama walevi wataimwaga damu ya maadui zao. Itatiririka kama damu ya tambiko iliyomiminwa madhabahuni kutoka bakulini. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, atawaokoa, maana wao ni kundi lake; nao watang'aa katika nchi yake kama mawe ya thamani katika taji. Jinsi gani uzuri na urembo wake ulivyo! Wavulana na wasichana watanawiri kwa wingi wa nafaka na divai mpya. Mwombeni Mwenyezi-Mungu awape mvua za masika. Mwenyezi-Mungu ndiye aletaye mawingu ya mvua; ndiye awapaye watu mvua za rasharasha, na kustawisha mimea shambani kwa ajili ya wote. Vinyago vyao vya kupigia ramli ni upuuzi mtupu, na waaguzi wao wanaagua uongo; watabiri wao wanatabiri ndoto za danganyifu, na kuwapa watu faraja tupu. Ndio maana watu wa Yuda wanatangatanga kama kondoo; wanataabika kwa kuwa wamekosa mchungaji. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nimewaka hasira dhidi ya hao wachungaji, nami nitawaadhibu hao viongozi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nitalitunza kundi langu, ukoo wa Yuda. Nitawafanya kuwa farasi wangu hodari wa vita. Kwa ukoo wa Yuda kutatokea: Watawala wa kila namna, viongozi imara kama jiwe kuu la msingi, walio thabiti kama kigingi cha hema, wenye nguvu kama upinde wa vita. Watu wa Yuda watakuwa kama mashujaa vitani watawakanyaga maadui zao katika tope njiani. Watapigana kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nipo pamoja nao; nao watawaaibisha hata wapandafarasi. “Watu wa Yuda nitawaimarisha; nitawaokoa wazawa wa Yosefu. Nitawarejesha makwao kwa maana nawaonea huruma, nao watakuwa kana kwamba sikuwa nimewakataa. Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, nami nitayasikiliza maombi yao. Watu wa Efraimu watakuwa kama mashujaa vitani; watajaa furaha kama waliokunywa divai. Watoto wao wataona hayo na kufurahi, watajaa furaha mioyoni kwa sababu yangu Mwenyezi-Mungu. “Nitawaita watu wangu na kuwakusanya pamoja; nimekusudia kuwakomboa, nao watakuwa wengi kama hapo awali. Japo niliwatawanya kati ya mataifa, hata hivyo, watanikumbuka wakiwa humo. Nao pamoja na watoto wao wataishi na kurudi majumbani mwao. Nitawarudisha kutoka nchini Misri, nitawakusanya kutoka Ashuru; nitawaleta nchini Gileadi na Lebanoni, nao watajaa kila mahali nchini. Watapitia katika bahari ya mateso, nami nitayapiga mawimbi yake, na vilindi vya maji ya mto Nili vitakauka. Kiburi cha Ashuru kitavunjwa na nguvu za Misri zitatoweka. Mimi nitawaimarisha watu wangu, nao watanitii na kuishi kwa kunipendeza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Fungua milango yako, ewe Lebanoni ili moto uiteketeze mierezi yako! Ombolezeni, enyi misunobari, kwa kuwa mierezi imeteketea. Miti hiyo mitukufu imeharibiwa! Enyi mialoni ya Bashani, ombolezeni, kwa kuwa msitu mnene umekatwa! Sikia maombolezo ya watawala! Fahari yao imeharibiwa! Sikia ngurumo za simba! Pori la mto Yordani limeharibiwa! Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, alisema hivi: “Jifanye mchungaji wa kondoo waendao kuchinjwa. Wanunuzi wao wanawachinja lakini hawaadhibiwi; na wauzaji wao wanasema, ‘Na ashukuriwe Mwenyezi-Mungu! Sasa tumetajirika’. Hata wachungaji wenyewe hawawaonei huruma. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba, sitawahurumia tena wakazi wa dunia. Nitamwacha kila mtu mikononi mwa mwenzake, na kila raia mikononi mwa mfalme wake. Nao wataiangamiza dunia, nami sitamwokoa yeyote mikononi mwao.” Basi, nikawa mchungaji wa kondoo waliokuwa wanakwenda kuchinjwa, kwani niliajiriwa na wale waliofanya biashara ya kondoo. Nikachukua fimbo mbili: Moja nikaiita “Fadhili,” na nyingine nikaiita “Umoja,” nikaenda kuchunga kondoo. Kwa muda wa mwezi mmoja, nikaua wachungaji watatu wabaya. Tena uvumilivu wangu kwa kondoo ukaniishia, nao kwa upande wao, wakanichukia. Basi, nikawaambia, “Sitakuwa mchungaji wenu tena. Atakayekufa na afe! Atakayeangamia na aangamie! Na wale watakaobaki na watafunane wao kwa wao.” Nikaichukua ile fimbo yangu niliyoiita “Fadhili,” nikaivunja, kuonesha kwamba agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na watu wake limevunjwa. Na agano hilo likavunjwa siku hiyohiyo. Wale wafanyabiashara ya kondoo waliokuwa wananiangalia, wakajua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa ameongea kwa matendo yangu. Kisha nikawaambia, “Kama mnaona kuwa ni sawa, nilipeni ujira wangu; lakini kama mnaona sivyo, basi kaeni nao.” Basi, wakanipimia vipande thelathini vya fedha mshahara wangu. Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Ziweke katika hazina ya hekalu.” Mshahara huo ulikuwa ni malipo halali kwa kazi yangu. Hivyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha, nikazitia katika hazina ya hekalu la Mwenyezi-Mungu. Kisha nikaivunja ile fimbo yangu ya pili niliyoiita “Umoja;” na hivyo nikauvunja umoja kati ya Yuda na Israeli. Mwenyezi-Mungu akaniambia tena, “Jifanye tena mchungaji, lakini safari hii uwe kama mchungaji mbaya! Maana nitaleta nchini mchungaji asiyemjali kondoo anayeangamia, au kumtafuta kondoo anayetangatanga, au kumtibu aliyejeruhiwa wala kumlisha aliye hai: Bali atakula wale kondoo wanono, hata kwato zao. “Ole wake mchungaji mbaya, ambaye anawaacha kondoo wake! Upanga na uukate mkono wake, na jicho lake la kulia na ling'olewe! Mkono wake na udhoofike, jicho lake la kulia na lipofuke.” Neno la Mwenyezi-Mungu kuhusu Israeli. Mwenyezi-Mungu aliyezitandaza mbingu, aliyeiweka misingi ya dunia na kumpa mwanadamu uhai asema hivi: “Nitaufanya mji wa Yerusalemu kuwa kama kikombe cha divai; na mataifa yaliyo kandokando yake yatakunywa na kuyumbayumba kama walevi. Mji wa Yerusalemu utakaposhambuliwa, hata miji yote ya Yuda itashambuliwa. Siku hiyo nitaufanya mji wa Yerusalemu kuwa kama jiwe zito kwa watu wote: Yeyote atakayelinyanyua atajiumiza mwenyewe. Watu wa mataifa yote duniani wataushambulia mji huo. Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, nitamtia hofu kila farasi, na mpandafarasi wake nitamfanya kuwa mwendawazimu. Farasi wa mataifa mengine nitawapofusha. Lakini kabila la Yuda nitalilinda. Ndipo viongozi wa Yuda watakapoambiana, ‘Wakazi wa Yerusalemu wamepata nguvu yao kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao’. “Siku hiyo, viongozi wa Yuda nitawafanya kama chungu cha moto mkali katika msitu; naam, kama mwenge uwakao kati ya miganda. Watayateketeza mataifa yote yaliyo kandokando yao. Lakini watu wa Yerusalemu wataendelea kuishi salama katika mji wao. “Nami Mwenyezi-Mungu nitawasaidia kwanza jamaa za Yuda kusudi wazawa wa Daudi na wakazi wa Yerusalemu wasijione kuwa maarufu zaidi ya watu wengine wa kabila la Yuda. Siku hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nitawalinda wakazi wa mji wa Yerusalemu; walio wanyonge zaidi miongoni mwao watakuwa na nguvu kama mfalme Daudi. Wazawa wa Daudi watashika usukani kuwaongoza watu wa Yuda kama malaika wangu mimi Mwenyezi-Mungu, naam, kama mimi Mungu mwenyewe. “Siku hiyo, nitayaangamiza mataifa yote yanayotaka kuushambulia mji wa Yerusalemu. Wazawa wa Daudi na wakazi wa mji wa Yerusalemu nitawajaza roho ya huruma na maombi, nao watamtazama yeye waliyemtoboa; watamlilia kama mtu amliliavyo mtoto wake wa pekee, au kama mtu amliliavyo kwa uchungu mzaliwa wake wa kwanza. Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu mjini Yerusalemu kama maombolezo ya kumwombolezea Hadad-rimoni katika mbuga za Megido. Nchi itaomboleza, kila ukoo utaomboleza peke yake, wanaume peke yao na wanawake peke yao; ukoo wa Daudi peke yake; ukoo wa Nathani peke yake; ukoo wa Lawi peke yake na ukoo wa Shimei peke yake. Jamaa zote zilizosalia zitaomboleza; wanaume peke yao na wanawake peke yao. “Siku hiyo, kutatokea chemchemi ya kuwatakasa dhambi na unajisi wazawa wa Daudi na wakazi wote wa Yerusalemu. Wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, majina ya vinyago vya miungu nchini nitayaondoa, wala hayatakumbukwa tena. Na wanaojidai kuwa manabii nitawaondolea mbali pamoja na tamaa zao za kuabudu sanamu. Mtu yeyote akijidai kuwa nabii, baba na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Unapaswa kufa kwa kuwa unasema uongo kwa jina la Mwenyezi-Mungu’. Na haohao wazazi wake watamchoma kisu akiwa anatabiri. Siku hiyo, kila nabii atayaonea aibu maono yake anapotabiri. Hawatavaa mavazi ya manyoya ili kudanganya watu, bali kila mmoja atasema, ‘Mimi si nabii. Mimi ni mkulima tu; nimeimiliki ardhi tangu ujana wangu’. Na mtu akimwuliza mmoja wao, ‘Vidonda hivi ulivyo navyo mgongoni vimetoka wapi?’ Yeye atajibu, ‘Vidonda hivi nilivipata katika nyumba ya rafiki zangu.’” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Amka, ee upanga! Inuka umshambulie mchungaji wangu; naam, mchungaji anayenitumikia. Mpige mchungaji na kondoo watawanyike. Nitaunyosha mkono wangu, kuwashambulia watu wadhaifu. Theluthi mbili za watu katika nchi zitaangamizwa; ni theluthi moja tu itakayosalimika. Theluthi hiyo moja itakayosalia, nitaijaribu na kuitakasa, kama mtu asafishavyo fedha, naam, kama ijaribiwavyo dhahabu. Hapo wao wataniomba mimi, nami nitawajibu. Nitasema, ‘Hawa ni watu wangu’, nao watasema, ‘Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu.’” Tazama, siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu inakuja. Siku hiyo, enyi watu wa Yerusalemu, mali yenu itagawanywa mbele ya macho yenu. Mwenyezi-Mungu atayakusanya mataifa yote ili kuushambulia mji wa Yerusalemu. Mji utatekwa, nyumba zenu zitatekwa nyara, na wanawake wenu watanajisiwa. Nusu ya wakazi wa mji watapelekwa uhamishoni, lakini nusu itakayosalia haitachukuliwa nje ya mji. Kisha Mwenyezi-Mungu atatoka na kuyapiga vita mataifa hayo, kama afanyavyo daima siku za vita. Siku hiyo, atasimama kwenye mlima wa mizeituni ulio mashariki ya mji wa Yerusalemu. Mlima huo utagawanywa sehemu mbili na bonde pana sana litatokea toka mashariki hadi magharibi. Nusu moja itaelekea kaskazini na nusu nyingine kusini. Nyinyi mtakimbia kupitia bonde hilo, katikati ya milima miwili ya Mwenyezi-Mungu. Mtakimbia kama wazee wenu walivyokimbia tetemeko la ardhi wakati wa utawala wa mfalme Uzia wa Yuda. Kisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, atakuja na watakatifu wote pamoja naye. Wakati huo hakutakuwa baridi wala baridi kali. Mchana utaendelea bila giza kuingia. Wakati huo wajulikana kwa Mwenyezi-Mungu peke yake. Hakutakuwa mchana wala usiku, kwa maana hata saa za jioni mwanga utaendelea kuwapo. Wakati huo, maji ya uhai yatabubujika kutoka mji wa Yerusalemu, na nusu ya maji hayo yatatiririkia kwenye bahari ya mashariki, na nusu nyingine kwenye bahari ya magharibi. Maji hayo yataendelea kububujika wakati wa kiangazi kama yalivyo wakati wa masika. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atakuwa ndiye mfalme pekee wa dunia yote; naye atakuwa ndiye Mwenyezi-Mungu pekee, mmoja tu, na jina lake litakuwa ndilo jina pekee. Nchi yote, tangu Geba hadi Rimoni, kusini mwa Yerusalemu, itageuzwa kuwa mbuga tambarare kabisa. Lakini mji wa Yerusalemu utabaki juu mahali pake tokea lango la Benyamini mpaka lango la zamani, hadi kwenye lango la Konani, tangu mnara wa Hanareli hadi kwenye mashinikizo ya mfalme. Mji wa Yerusalemu utakaliwa na watu kwani ndani yake haitakuwapo laana tena; naam, watu watakaa humo kwa usalama. Lakini kuhusu wale watu ambao walikuja kupigana na Yerusalemu, haya ndiyo maafa ambayo Mwenyezi-Mungu atawaletea: Miili yao itaoza wangali hai; macho yao yataoza yakiwa kwenye matundu yake na ndimi zao zitaoza zikiwa vinywani mwao. Siku hiyo, hofu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu itawakumba watu, na kila mtu atamshambulia mwenzake. Watu wa Yuda watapigana kuulinda mji wa Yerusalemu; utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka nchi ya Yuda utakusanywa: Watakusanya dhahabu, fedha na mavazi kwa wingi sana. Maafa makubwa yatawakumba farasi, nyumbu, ngamia, punda na wanyama wote watakaokuwamo katika kambi hizo za maadui. Kisha, kila mtu aliyesalimika kati ya mataifa yote yaliyokuja kuushambulia mji wa Yerusalemu, atakuwa akija Yerusalemu mwaka hata mwaka, kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, na kuadhimisha sikukuu ya vibanda. Iwapo taifa lolote duniani halitakwenda Yerusalemu kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, basi, mvua haitanyesha katika nchi yao. Iwapo Wamisri watakataa kuiadhimisha sikukuu ya vibanda, basi, Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa ugonjwa uleule atakaowapiga nao mataifa yote yanayokataa kuiadhimisha sikukuu hiyo. Hiyo itakuwa ndiyo adhabu itakayolipata taifa la Misri pamoja na mataifa yote yasiyoadhimisha sikukuu ya vibanda. Wakati huo, kwenye njuga za farasi yataandikwa maandishi haya: “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu Vyungu vilivyomo katika hekalu la Mwenyezi-Mungu vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu. Kila chungu katika mji wa Yerusalemu na nchi ya Yuda kitawekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ili wote wanaotoa tambiko waweze kuvichukua na kuchemshia nyama ya tambiko. Wakati huo, hakutakuwapo mfanya biashara yeyote katika hekalu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Kauli ya Mwenyezi-Mungu iliyomjia Malaki awaambie Waisraeli. Mwenyezi-Mungu asema: “Daima nimewapenda nyinyi”. Lakini watu wa Israeli wanauliza, “Umetupendaje?” Naye Mwenyezi-Mungu asema: “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nilimpenda Yakobo nikamchukia Esau. Nimeiharibu nchi ya milima ya Esau ambayo ni urithi wake, nikawaachia mbwamwitu wa jangwani. Nao wazawa wa Esau, yaani Waedomu, wanasema kwamba ingawa miji yao imeharibiwa, watajenga upya magofu yake. Lakini, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema kwamba wanaweza kuijenga upya, lakini mimi nitaibomolea mbali. Watu watawaita, ‘Taifa ovu ambalo Mwenyezi-Mungu amelikasirikia milele.’ Nanyi mtakapoyaona hayo kwa macho yenu, mtatambua na kusema: ‘Ukuu wa Mwenyezi-Mungu wafika hata nje ya mipaka ya nchi ya Israeli.’” Mwenyezi-Mungu wa majeshi anawaambia hivi nyinyi makuhani mnaolidharau jina lake: “Mtoto humheshimu mzazi wake, na mtumishi humheshimu bwana wake. Ikiwa mimi ndiye Baba yenu, mbona mwanivunjia heshima? Ikiwa mimi ni bwana wenu, mbona hamniheshimu? Nanyi mnauliza, ‘Sisi tumekudharauje?’ Mwanidharau kwa kunitolea madhabahuni pangu tambiko ya chakula najisi. Lakini nyinyi mnauliza, ‘Tumekitiaje najisi?’ Mnakitia najisi kwa kuidharau madhabahu yangu. Mnaponitolea tambiko ya mnyama kipofu, au kilema, au mgonjwa, je, huo si uovu? Je, mtawala atapendezwa au kukufanyia hisani ukimpa zawadi ya mnyama kama huyo?” Kwa hiyo sasa enyi makuhani, mwombeni Mungu ili atuhurumie. Ikiwa mnamtolea matoleo ya aina hiyo, je, kweli atakuwa radhi nanyi? Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema, “Laiti angepatikana mtu mmoja miongoni mwenu ambaye angefunga milango ya hekalu ili msiwashe moto usiokubalika kwenye madhabahu yangu! Sipendezwi nanyi na sitaikubali tambiko yoyote mnayonitolea. Watu wa mataifa kote duniani, toka mawio ya jua hadi machweo yake, wanalitukuza jina langu. Kila mahali wananifukizia ubani na kunitolea tambiko zinazokubalika; maana jina langu linatukuzwa miongoni mwao. Lakini nyinyi mnalibeza jina langu pale mnapoichafua madhabahu yangu, na chakula mnachotoa juu yake mnakidharau. Mnasema, ‘Mambo haya yametuchosha mno,’ na mnanidharau. Mnaniletea tambiko za wanyama mliowapata kwa unyang'anyi, au walio vilema au wagonjwa. Je, nipokee tambiko hizo mikononi mwenu? Mimi Mwenyezi-Mungu nauliza. Na alaaniwe mtu yeyote anidanganyaye, ambaye huahidi kwa kiapo kunitolea tambiko mnyama safi kutoka katika kundi lake, lakini hunitolea tambiko mnyama mwenye kilema. Tazama, mimi ni mfalme mkuu, na watu wa mataifa yote hunicha.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi awaambia makuhani: “Sasa enyi makuhani, nawaamuruni hivi: Ni lazima mniheshimu mimi kwa matendo yenu, msiponisikiliza nitawaleteeni laana, vitu vyote mnavyopewa kwa mahitaji yenu nitavilaani. Na kweli nimekwisha kuvilaani, kwa sababu hamuyatilii maanani maagizo yangu. Tazama, nitawaadhibu watoto wenu na nyinyi wenyewe kutokana na uovu wenu, na kuzipaka nyuso zenu mavi ya wanyama wenu wa tambiko. Nitawafukuza mbali nami. Hivyo mtajua kuwa nimewapeni amri hii ili agano langu na ukoo wa Lawi liwe la kudumu. “Katika agano hilo, niliwaahidi uhai na amani na kwamba wao ni lazima kunicha mimi, nao kwa upande wao walinicha mimi, wakaliogopa jina langu. Mafundisho yao yalikuwa ya kweli na kamwe hawakufundisha uongo. Mimi na wao tulikaa kwa amani. Si kwamba walitenda haki tu, bali waliwafundisha wengine kutotenda maovu. Ni wajibu wa makuhani kuwafundisha watu maarifa ya kweli juu ya Mungu. Watu wawaendee kujifunza matakwa yangu kwao, kwani makuhani ni wajumbe wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. “Bali nyinyi makuhani mmegeuka mkaiacha njia ya haki. Mafundisho yenu yamewaongoza watu wengi katika kutenda mabaya. Mmelivunja agano nililofanya nanyi. Nami pia nitawafanya mdharauliwe na kupuuzwa na Waisraeli, kwa sababu hamkuzifuata njia zangu, na mnapowafundisha watu wangu mnapendelea baadhi yao.” Je, sisi sote si watoto wa baba mmoja? Je, sisi sote hatukuumbwa na Mungu yuleyule? Mbona basi, hatuaminiani sisi kwa sisi, na tunalidharau agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na wazee wetu? Watu wa Yuda wamekosa uaminifu kwa Mungu na kutenda machukizo katika Israeli na mjini Yerusalemu. Wamelitia unajisi hekalu la Mwenyezi-Mungu analolipenda. Tena wameoa wanawake wanaoabudu miungu ya kigeni. Mwenyezi-Mungu na awaondolee mbali watu wanaofanya mambo hayo kutoka miongoni mwa wazawa wa Yakobo. Na kamwe wasishiriki katika kutoa ushuhuda na kuleta tambiko mbele ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Zaidi ya hayo yote, mnaifunika madhabahu ya Mwenyezi-Mungu kwa machozi yenu, mkilia na kuomboleza kwa sababu yeye hazikubali tena tambiko mnazomtolea. Mnauliza, “Mbona sasa hazikubali?” Mwenyezi-Mungu hazikubali kwa sababu anajua wazi kuwa umeivunja ahadi yako kwa mke wa ujana wako. Umekosa uaminifu kwake ingawa uliahidi mbele ya Mungu kwamba ungekuwa mwaminifu kwake. Je, Mungu hakuwafanya nyote wawili muwe mwili mmoja na roho moja? Je, alikusudia nini alipofanya hayo? Yamkini alikusudia tuzae watoto ambao watamcha yeye. Kwa hiyo, hakikisheni kuwa hakuna hata mmoja wenu anayekosa uaminifu kwa mkewe. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli asema: “Ninachukia talaka. Ninachukia mmoja wenu anapomtendea mkewe ukatili huo. Hakikisheni kwamba hakuna hata mmoja wenu anayekosa uaminifu kwa mkewe.” Mmemchosha Mwenyezi-Mungu kwa maneno yenu matupu. Hata hivyo, mnasema, “Tumemchoshaje?” Mmemchosha mnaposema, “Mwenyezi-Mungu huwaona kuwa wema watu wanaotenda maovu; tena anawapenda.” Au mnapouliza, “Yuko wapi yule Mungu mwenye haki?” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema, “Tazama, namtuma mjumbe wangu anitangulie kunitayarishia njia. Bwana mnayemtafuta atalijia hekalu lake ghafla. Mjumbe mnayemtazamia kwa hamu kubwa atakuja na kutangaza agano langu.” Lakini ni nani atakayestahimili siku hiyo atakapokuja? Ni nani atakayesimama kustahimili atakapotokea? Yeye ni kama moto mkali usafishao chuma; ni kama sabuni ya dobi. Yeye atakuja kuhukumu kama mtu asafishaye na kutakasa fedha. Atawasafisha wazawa wa Lawi, kama mtu afuavyo dhahabu au fedha, mpaka wamtolee Mwenyezi-Mungu tambiko zinazokubalika. Hivyo, tambiko za watu wa Yuda na wa Yerusalemu zitampendeza Mwenyezi-Mungu kama za watu wa kale; kama katika miaka ya zamani. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Kisha nitawakaribia ili kuwahukumu. Sitasita kutoa ushahidi dhidi ya wachawi, wazinzi, watoa ushahidi wa uongo, wanaowapunja waajiriwa, wanaowadhulumu wageni na wale wasionicha mimi. “Mimi ni Mwenyezi-Mungu, mimi sibadiliki. Lakini nyinyi, nyinyi wazawa wa Yakobo hamjatoweka bado. Tangu wakati wa wazee wenu, mmezidharau kanuni zangu wala hamkuzifuata. Basi, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu nasema: Nirudieni, nami nitawageukieni. Lakini nyinyi mnauliza, ‘Tutakurudia namna gani?’ Nami nawaulizeni, Je, ni sawa mtu kumdanganya Mungu? La! Lakini nyinyi mnanidanganya! Walakini nyinyi mwauliza: ‘Tunakudanganya kwa namna gani?’ Naam! Mnanidanganya kuhusu zaka na tambiko zenu. Nyinyi na taifa lenu lote mmelaaniwa kwa sababu ya kunidanganya. Leteni ghalani mwangu zaka yote, ili nyumbani mwangu kuwe na chakula cha kutosha. Kisha mwaweza kunijaribu. Nijaribuni namna hiyo nanyi mtaona kama sitayafungua madirisha ya mbinguni na kuwatiririshia baraka tele. Wadudu waharibifu nitawakemea wasiyaharibu tena mazao yenu. Mizabibu yenu mashambani haitaacha kuzaa matunda. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Ndipo mataifa yote yatawaita nyinyi watu waliobarikiwa, maana nchi yenu itakuwa nchi ya furaha. Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Maneno yenu yamekuwa mzigo kwangu. Hata hivyo mnasema, ‘Tumesema nini dhidi yako?’ Nyinyi mmesema, ‘Kumtumikia Mungu hakuna faida. Kuna faida gani kuyatii maagizo ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi, au kujaribu kumwonesha kuwa tumekosa mbele yake kwa kutembea kama watu wanaoomboleza? Tuonavyo sisi, ni kwamba, wenye kiburi ndio wenye furaha daima. Watu waovu, licha ya kustawi, hata wanapomjaribu Mungu, hawapati adhabu.’” Ndipo watu wanaomcha Mwenyezi-Mungu walipozungumza wao kwa wao, naye Mwenyezi-Mungu akasikia mazungumzo yao. Mbele yake kikawekwa kitabu ambamo iliandikwa kumbukumbu ya wale wanaomcha na kumheshimu. Iliandikwa hivi: Mwenyezi-Mungu asema: “Hao watakuwa watu wangu. Watakuwa urithi wangu maalumu siku ile nitakapoinuka kufanya ninalokusudia. Sitawadhuru kama vile baba asivyomdhuru mwanawe anayemtumikia. Hapo ndipo mtakapotambua tena tofauti iliyopo kati ya waadilifu na waovu; naam, kati ya mtu anayemtumikia Mungu na asiyemtumikia.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Tazama, siku yaja, nayo inawaka kama tanuri. Wenye kiburi na waovu wote watatupwa humo na kuteketea kama mabua makavu; watateketea kabisa pasibaki hata alama. Lakini kwa ajili yenu nyinyi mnaonicha, uwezo wangu wa kuokoa utawachomozea kama jua lililo na nguvu za kuponya kwenye mionzi yake. Mtatoka mkirukaruka kama ndama watokapo zizini mwao. Siku hiyo mtawakanyagakanyaga waovu, nao watakuwa kama majivu chini ya nyayo zenu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi. “Kumbukeni sheria, kanuni na maagizo yangu niliyomwamuru Mose mtumishi wangu kule mlimani Horebu, ili awaamuru watu wote wa Israeli. “Tazama, kabla ya kufika siku ile kuu na ya kutisha, nitamtuma nabii Elia. Nabii Elia atawapatanisha wazazi na watoto wao; la sivyo, nitakuja na kuiangamiza nchi yenu.” Yesu Kristo alikuwa wa ukoo wa Daudi, wa ukoo wa Abrahamu. Hii ndiyo orodha ya ukoo wake: Abrahamu alimzaa Isaka, Isaka alimzaa Yakobo, Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake, Yuda alimzaa Peresi na Zera (mama yao alikuwa Tamari), Peresi alimzaa Hesroni, Hesroni alimzaa Rami, Rami alimzaa Aminadabu, Aminadabu alimzaa Nashoni, Nashoni alimzaa Salmoni, Salmoni alimzaa Boazi (mama yake Boazi alikuwa Rahabu) Boazi na Ruthu walikuwa wazazi wa Obedi, Obedi alimzaa Yese, naye Yese alimzaa Mfalme Daudi. Daudi alimzaa Solomoni (mama yake Solomoni alikuwa Bath-Sheba mke wa Uria). Solomoni alimzaa Rehoboamu, Rehoboamu alimzaa Abiya, Abiya alimzaa Asa, Asa alimzaa Yehoshafati, Yehoshafati alimzaa Yoramu, Yoramu alimzaa Uzia, Uzia alimzaa Yothamu, Yothamu alimzaa Ahazi, Ahazi alimzaa Hezekia, Hezekia alimzaa Manase, Manase alimzaa Amoni, Amoni alimzaa Yosia, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake. Huo ulikuwa wakati Wayahudi walipopelekwa uhamishoni Babuloni. Baada ya Wayahudi kupelekwa uhamishoni Babuloni, Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli alimzaa Zerubabeli, Zerubabeli alimzaa Abiudi, Abiudi alimzaa Eliakimu, Eliakimu alimzaa Azori, Azori alimzaa Zadoki, Zadoki alimzaa Akimu, Akimu alimzaa Eliudi, Eliudi alimzaa Eleazari, Eleazari alimzaa Mathani, Mathani alimzaa Yakobo, Yakobo alimzaa Yosefu, mumewe Maria mama yake Yesu aitwaye Kristo. Basi, kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo. Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri. Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, “Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye ndiye atakayewaokoa watu wake katika dhambi zao.” Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii: “Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, nao watampa jina Emanueli” (maana yake, “Mungu yuko nasi”). Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani. Lakini hakulala naye hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu. Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu, wakauliza, “Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu.” Mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu. Basi, akawaita pamoja makuhani wakuu wote na waalimu wa sheria, akawauliza, “Kristo atazaliwa wapi?” Nao wakamjibu, “Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika: ‘Ee Bethlehemu nchini Yudea, wewe si mdogo kamwe kati ya miji maarufu ya Yudea; maana kwako atatokea kiongozi atakayewaongoza watu wangu, Israeli.’” Hapo, Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile nyota ilipowatokea. Kisha akawatuma Bethlehemu akisema, “Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende kumwabudu.” Baada ya kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali pale alipokuwa mtoto. Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno. Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: Dhahabu, ubani na manemane. Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine. Baada ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapokuambia, maana Herode anakusudia kumuua huyu mtoto.” Hivyo, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda Misri. Akakaa huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana kwa njia ya nabii litimie: “Nilimwita Mwanangu kutoka Misri.” Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia: “Sauti imesikika huko Rama, kilio na maombolezo mengi. Raheli anawalilia watoto wake, wala hataki kutulizwa, maana wote wamefariki.” Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumuua mtoto huyo wamekwisha kufa.” Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea nchini Israeli. Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao, mwanawe Herode, alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye, baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda pande za Galilaya, akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: “Ataitwa Mnazare.” Siku zile Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri katika jangwa la Yudea: “Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema: “Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake, nyosheni barabara zake.’” Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka pande zote za Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia ili awabatize, aliwaambia, “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea muikimbie ghadhabu inayokuja? Onesheni kwa vitendo kwamba mmetubu. Msifikiri na kujisemea, ‘Baba yetu ni Abrahamu!’ Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu. Basi, shoka liko tayari kwenye mizizi ya miti; hivyo, kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni. Mimi ninawabatizeni kwa maji kuonesha mmetubu. Lakini anayekuja baada yangu ana nguvu kuliko mimi, nami sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Yeye anashika mkononi chombo cha kupuria nafaka, ili aipure nafaka yake; akusanye ngano yake ghalani, na makapi ayachome kwa moto usiozimika.” Wakati huo Yesu alitoka Galilaya akafika katika mto Yordani, akamwendea Yohane ili abatizwe naye. Lakini Yohane alijaribu kumzuia akisema, “Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe.” Lakini Yesu akamjibu, “Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana ndivyo inavyofaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka.” Hapo Yohane akakubali. Mara tu Yesu alipokwisha batizwa, alitoka majini; na kumbe mbingu zikafunguka, akaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa na kutua juu yake. Sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ndiye Mwanangu mpendwa, nimependezwa naye.” Kisha Roho alimwongoza Yesu mpaka jangwani ili ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arubaini mchana na usiku, na mwishowe akaona njaa. Basi, mshawishi akamjia, akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.” Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno asemalo Mungu.’” Kisha Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu, akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini; maana imeandikwa: ‘Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe.’” Yesu akamwambia, “Imeandikwa pia: ‘Usimjaribu Bwana, Mungu wako.’” Kisha Ibilisi akamchukua mpaka juu ya mlima mrefu, akamwonesha falme zote za ulimwengu na fahari zake, akamwambia, “Hivi vyote nitakupa kama ukipiga magoti na kuniabudu.” Hapo, Yesu akamwambia, “Nenda zako Shetani! Imeandikwa: ‘Utamwabudu Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye peke yake.’” Basi, Ibilisi akamwacha, na malaika wakaja, wakamhudumia. Yesu aliposikia kwamba Yohane ametiwa gerezani alikwenda Galilaya. Aliondoka Nazareti, akaenda Kafarnaumu, mji ulio kando ya bahari ya Genesareti, mpakani mwa wilaya za Zebuluni na Naftali, akakaa huko. Ndivyo lilivyotimia lile neno lililosemwa kwa njia ya nabii Isaya: “Nchi ya Zebuluni na nchi ya Naftali, kuelekea baharini ngambo ya mto Yordani, Galilaya, nchi ya watu wa mataifa! Watu waliokaa gizani wameona mwanga mkubwa. Nao walioishi katika nchi ya giza na kivuli cha kifo, mwanga umewaangazia!” Tangu wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, “Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekariia!” Yesu alipokuwa anatembea kando ya ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili wavuvi; Simoni (aitwaye Petro) na Andrea, ndugu yake; walikuwa wakivua samaki kwa nyavu ziwani. Basi, akawaambia, “Nifuateni, nami nitawafanya nyinyi wavuvi wa watu.” Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona ndugu wengine wawili: Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Hao walikuwa ndani ya mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakitengeneza nyavu zao. Basi, Yesu akawaita, nao mara wakaiacha mashua pamoja na baba yao, wakamfuata. Yesu alikuwa anakwenda kila mahali wilayani Galilaya, akifundisha katika masunagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu. Habari zake zikaenea pande zote za Siria. Wagonjwa wote wenye maradhi ya kila namna na wale waliosumbuliwa na kila namna ya taabu: Waliopagawa na pepo, wenye kifafa na watu waliokuwa wamelemaa, walipelekwa kwake; naye akawaponya wote. Makundi mengi ya watu kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea na ngambo ya mto Yordani, yalimfuata. Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda mlimani, akaketi. Wanafunzi wake wakamwendea, naye akaanza kuwafundisha: “Heri walio maskini rohoni, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa. Heri walio wapole, maana watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana watashibishwa. Heri walio na huruma, maana watahurumiwa. Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu. Heri wenye kuleta amani, maana wataitwa watoto wa Mungu. Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu, maana ufalme wa mbinguni ni wao. “Heri yenu nyinyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu. “Nyinyi ni chumvi ya dunia. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na nini? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu. “Nyinyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika. Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni. “Msidhani kuwa nimekuja kutangua sheria na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha. Kweli nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au sehemu ndogo kabisa ya sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia. Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Ndio maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa waalimu wa sheria na wa Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. “Mmekwisha sikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: ‘Usiue! Atakayeua lazima ahukumiwe.’ Lakini mimi nawaambieni, yeyote anayemkasirikia ndugu yake, lazima ahukumiwe. Anayemdharau ndugu yake atapelekwa mahakamani. Anayemwita ndugu yake: ‘Pumbavu’ atastahili kuingia katika moto wa Jehanamu. “Basi, ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako ana ugomvi nawe, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo urudi utoe sadaka yako. “Patana na mshtaki wako upesi mkiwa bado njiani kwenda mahakamani. La sivyo, mshtaki wako atakukabidhi kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa askari, nawe utafungwa gerezani. Kweli nakuambia, hutatoka humo mpaka umelipa senti ya mwisho. “Mmesikia kwamba watu waliambiwa: ‘Usizini!’ Lakini mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake. Basi, kama jicho lako la kulia linakukosesha, lingoe ukalitupe mbali. Afadhali zaidi kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa katika moto wa Jehanamu. Na kama mkono wako wa kulia unakukosesha, ukate ukautupe mbali. Afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote uende katika moto wa Jehanamu. “Ilikwisha semwa pia: ‘Anayemwacha mke wake, yampasa ampe hati ya talaka’. Lakini mimi nawaambieni, anayempa mkewe talaka, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, anamfanya azini; na mwanamume akimwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini. “Tena mmesikia kwamba watu wa kale waliambiwa: ‘Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana.’ Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Ukisema, ‘Ndiyo’, basi iwe ‘Ndiyo’; ukisema, ‘Siyo’, basi iwe kweli ‘Siyo’. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu. “Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino.’ Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia la pili. Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti lako. Mtu akikulazimisha kubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili. Akuombaye mpe, wala usimpe kisogo anayetaka kukukopa kitu. “Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Mpende jirani yako, na kumchukia adui yako.’ Lakini mimi nawaambieni, wapendeni maadui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu nyinyi, ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu. Je, mtapata tuzo gani kwa kuwapenda tu wale wanaowapenda nyinyi? Hakuna! Kwa maana, hata watozaushuru hufanya hivyo! Kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mmefanya kitu kisicho cha kawaida? Hata watu wasiomjua Mungu nao hufanya vivyo hivyo. Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. “Jihadharini msije mkafanya matendo yenu mema mbele ya watu kusudi mwonekane nao. La sivyo, Baba yenu aliye mbinguni hatawapeni tuzo. “Basi, unapomsaidia maskini, usijitangaze. Usifanye kama wanafiki wafanyavyo katika masunagogi na njiani ili watu wawasifu. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. Lakini wewe unapomsaidia maskini, fanya hivyo kwamba hata mwandani wako asijue ufanyalo. Toa msaada wako kwa siri, na Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza. “Mnaposali, msifanye kama wanafiki. Wao hupenda kusimama na kusali katika masunagogi na katika pembe za njia ili watu wawaone. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango, kisha umwombe Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza. “Mnaposali, msipayuke maneno kama watu wasiomjua Mungu. Wao hudhani kwamba Mungu atawasikiliza ati kwa sababu ya maneno mengi. Msiwe kama wao. Baba yenu anajua mnayoyahitaji hata kabla ya kumwomba. Basi, hivi ndivyo mnavyopaswa kusali: ‘Baba yetu uliye mbinguni: Jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Utupe leo chakula chetu cha kila siku. Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea. Usitutie katika majaribu, lakini utuokoe na yule Mwovu.’ [ Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] “Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia. Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu. “Mnapofunga, msiwe na huzuni kama wanafiki. Wao hukunja nyuso zao wapate kuonekana na watu kuwa wanafunga. Nawaambieni kweli, hao wamekwisha pata tuzo lao. Wewe lakini unapofunga, paka kichwa chako mafuta, nawa uso wako, ili mtu yeyote asijue kwamba unafunga, ila ujulikane tu kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza. “Msijiwekee hazina hapa duniani ambako nondo na kutu huharibu, na wezi huingia na kuiba. Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuiharibu, wala wezi hawaingii wakaiba. Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako. “Jicho ni taa ya mwili. Kama basi jicho lako ni zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Lakini ikiwa jicho lako ni bovu, mwili wako wote utakuwa katika giza. Basi, ikiwa mwanga uliomo ndani yako ni giza, basi, hilo ni giza la kutisha mno! “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili. Maana atamchukia mmoja na kumpenda huyo wa pili; au ataambatana na mmoja na kumdharau huyo mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali pamoja. “Ndiyo maana nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula na kinywaji mnavyohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Je, maisha ni chakula tu au zaidi? Na mwili, je, si zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa mwituni: Hawapandi, hawavuni, wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, nyinyi si wa thamani kuliko hao? Ni nani miongoni mwenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuuongeza muda wa maisha yake? “Na kuhusu mavazi, ya nini kuwa na wasiwasi? Tazameni maua ya porini jinsi yanavyostawi. Hayafanyi kazi wala hayasokoti. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba! “Basi, msiwe na wasiwasi: ‘Tutakula nini, tutakunywa nini, tutavaa nini!’ Maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wasiomjua Mungu. Baba yenu wa mbinguni anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo vyote. Bali, shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu na matakwa yake, na hayo yote mtapewa kwa ziada. Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo. “Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu; kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu. Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako? Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyomo jichoni mwako na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichomo jichoni mwa ndugu yako. “Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua nyinyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga. “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni mlango, nanyi mtafunguliwa. Maana, yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye mlango hufunguliwa. Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe? Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka? Kama basi nyinyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: Atawapa mema wale wanaomwomba. “Yote mnayotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. Hii ndiyo maana ya sheria ya Mose na mafundisho ya manabii. “Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi. Lakini njia inayoongoza kwenye uhai ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo. “Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali. Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La! Basi, mti mzuri huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni. Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao. “Si kila aniambiaye, ‘Bwana, Bwana’, ataingia katika ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza matakwa ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile ya hukumu: ‘Bwana, Bwana! Kwa jina lako tulitangaza ujumbe wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi’. Hapo nitawaambia: ‘Sikuwajua nyinyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu.’ “Kwa hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba. “Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga. Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaanguka; tena anguko hilo lilikuwa kubwa.” Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake. Hakuwa kama waalimu wao wa sheria, bali alifundisha kwa mamlaka. Yesu aliposhuka mlimani, makundi mengi ya watu yalimfuata. Basi, akaja mtu mmoja mwenye ukoma, akamsujudia na kusema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa!” Yesu akanyosha mkono, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika.” Mara huyo mtu akapona ukoma wake. Kisha Yesu akamwambia, “Angalia, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani, na kutoa sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba umepona.” Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, jemadari mmoja alimwendea, akamsihi akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana.” Yesu akamwambia, “Nitakuja kumponya.” Huyo jemadari akamwambia, “Bwana, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; na mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.” Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, “Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli mwenye imani kama hii. Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. Lakini wale ambao ufalme huo ni wao watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno.” Kisha Yesu akamwambia huyo jemadari Mroma, “Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini.” Na mtumishi wake akapona saa ileile. Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali. Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia. Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa. Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: “Yeye mwenyewe ameuchukua udhaifu wetu, ameyabeba magonjwa yetu.” Yesu alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ngambo ya ziwa. Mwalimu mmoja wa sheria akamwendea, akamwambia, “Mwalimu, mimi nitakufuata kokote utakakokwenda.” Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia.” Kisha mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu.” Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao.” Yesu alipanda mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye. Mara, dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu lakini alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wakamwendea, wakamwamsha wakisema, “Bwana, tuokoe, tunaangamia!” Yesu akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?” Basi, akainuka, akaukemea upepo na lile ziwa; kukawa shwari kabisa. Watu wakashangaa, wakasema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na bahari vinamtii!” Yesu alifika katika nchi ya Wagadara, ngambo ya ziwa, na huko watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitokea makaburini. Watu hawa walikuwa wenye kutisha mno, hata hakuna mtu aliyethubutu kupita njia hiyo. Nao wakaanza kupiga kelele, “Una shauri gani nasi, wewe Mwana wa Mungu? Je, umekuja kututesa kabla ya wakati wake?” Karibu na mahali hapo kulikuwa na nguruwe wengi wakichungwa. Basi, hao pepo wakamsihi, “Ikiwa utatutoa, basi uturuhusu tuwaingie nguruwe wale.” Yesu akawaambia, “Haya, nendeni.” Hapo wakawatoka watu hao, wakawaingia nguruwe. Kundi lote la nguruwe likaporomoka kwenye ule mteremko mkali, likatumbukia ziwani; nguruwe wote wakafa majini. Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakaenda mjini. Huko walitoa habari zote na mambo yaliyowapata wale watu waliokuwa wamepagawa. Basi, watu wote katika mji ule walitoka, wakamwendea Yesu; na walipomwona, wakamsihi aondoke katika nchi yao. Yesu alipanda mashua, akavuka ziwa na kufika katika mji wake. Hapo watu walimletea mtu mmoja aliyepooza mwili, amelazwa juu ya kitanda. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Jipe moyo mwanangu! Umesamehewa dhambi zako.” Baadhi ya waalimu wa sheria wakaanza kufikiri, “Mtu huyu anamkufuru Mungu!” Yesu aliyajua mawazo yao, akasema, “Kwa nini mnawaza mabaya mioyoni mwenu? Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Simama, utembee?’ Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo duniani wa kuwasamehe watu dhambi.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Inuka, chukua kitanda chako, uende nyumbani kwako.” Huyo mtu aliyekuwa amepooza akainuka, akaenda nyumbani kwake. Watu wote katika ule umati walipoona hayo, walishangaa na kuogopa; wakamtukuza Mungu aliyewapa binadamu uwezo wa namna hiyo. Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda zake, alimwona mtu mmoja aitwaye Mathayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Basi, Yesu akamwambia, “Nifuate.” Naye Mathayo akainuka, akamfuata. Yesu alipokuwa nyumbani ameketi kula chakula, watozaushuru wengi na wahalifu walikuja wakaketi pamoja naye na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona hayo, wakawaambia wanafunzi wake, “Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?” Yesu aliwasikia, akasema, “Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: ‘Nataka huruma, wala si tambiko.’ Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi.” Kisha wanafunzi wa Yohane Mbatizaji walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Sisi na Mafarisayo hufunga mara nyingi; mbona wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akawajibu, “Je, walioalikwa harusini hutakiwa kuomboleza wakati bwana arusi yupo pamoja nao? La, hasha! Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga. “Watu hawatii kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu. Maana kiraka hicho kitararua hilo vazi kuukuu, na pale palipokuwa pameraruka pataongezeka. Wala watu hawaweki divai mpya katika viriba vikuukuu. Wakifanya hivyo, viriba hupasuka na divai ikamwagika, navyo viriba vikaharibika. Ila, watu huweka divai mpya katika viriba vipya, na vyote viwili, viriba na divai, vikahifadhiwa salama.” Yesu alipokuwa akisema hayo, ofisa mmoja Myahudi alifika, akamwinamia na kusema, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini, tafadhali twende umwekee mkono wako naye ataishi.” Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake, akamfuata. Mama mmoja, mgonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. Alifanya hivyo kwani alifikiri moyoni: “Nikigusa tu vazi lake, nitapona.” Basi, Yesu akageuka akamwona, akamwambia, “Binti, jipe moyo! Imani yako imekuponya.” Mama huyo akapona saa ileile. Kisha Yesu akaingia nyumbani kwa yule ofisa. Na alipowaona wapiga filimbi na umati wa watu wanaoomboleza, akasema, “Ondokeni hapa! Msichana huyu hakufa, amelala tu.” Nao wakamcheka. Basi, umati wa watu ulipoondolewa, Yesu aliingia ndani, akamshika huyo msichana mkono, naye akasimama. Habari hiyo ikavuma sana katika nchi ile yote. Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda, vipofu wawili walimfuata wakipiga kelele, “Mwana wa Daudi, utuhurumie!” Yesu alipoingia nyumbani, watu hao wawili wakamwendea, naye akawauliza, “Je, mnaamini kwamba naweza kuwafanyia jambo hilo?” Nao wakamjibu, “Naam, Bwana.” Hapo Yesu akayagusa macho yao, akasema, “Na iwe kwenu kama mnavyoamini.” Macho yao yakafunguliwa. Naye Yesu akawaonya kwa ukali: “Msimwambie mtu yeyote jambo hili.” Lakini wao wakaondoka, wakaeneza habari za Yesu katika nchi ile yote. Watu walipokuwa wanakwenda zao, wengine walimletea Yesu mtu mmoja aliyekuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Mara tu huyo pepo alipotolewa, mtu huyo aliyekuwa bubu akaanza kuongea tena. Watu wakashangaa na kusema, “Jambo kama hili halijapata kuonekana katika Israeli!” Lakini Mafarisayo wakawa wanasema, “Anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo wabaya.” Yesu alitembelea miji yote na vijiji, akafundisha katika masunagogi yao akihubiri Habari Njema ya ufalme wa Mungu, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila namna. Basi, alipowaona watu, makundi kwa makundi, aliwaonea huruma kwa sababu walikuwa hoi na wenye wasiwasi kama kondoo wasio na mchungaji. Hapo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi, lakini wafanyakazi ni wachache. Basi mwombeni mwenye mavuno atume wafanyakazi wavune mavuno yake.” Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kuwafukuza pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote. Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: Wa kwanza ni Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake; Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtozaushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu. Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: “Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika miji ya Wasamaria. Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo. Mnapokwenda hubirini hivi: ‘Ufalme wa mbinguni umekaribia.’ Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure. Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba. Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake. “Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu anayestahili kutembelewa, na kaeni huko mpaka mtakapoondoka mahali hapo. Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake. Kama wenyeji wa nyumba hiyo wanastahili salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawastahili, basi amani yenu itawarudia nyinyi. Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakunguteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao. Kweli nawaambieni, siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora. “Sasa, mimi nawatuma nyinyi kama kondoo kati ya mbwamwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa. Jihadharini na watu, maana watawapeleka nyinyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kunishuhudia kwao na kwa watu wa mataifa. Basi, watakapowapeleka nyinyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema. Maana si nyinyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. “Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokolewa. “Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika. “Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumishi hampiti bwana wake. Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je, hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi? “Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa. Ninalowaambieni nyinyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinongonezwa, litangazeni hadharani. Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu. Shomoro wawili huuzwa kwa sarafu moja ndogo. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu. Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Kwa hiyo msiogope; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi. “Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. Lakini yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. “Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. Maana nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama yake, kati ya mkwe na mkwe wake. Na maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake. “Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili. Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. “Anayewapokea nyinyi, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. Anayempokea nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii. Anayempokea mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema. Kweli nawaambieni, yeyote atakayempa mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi kwa sababu ni mfuasi wangu, hakika hatakosa kamwe kupata tuzo lake.” Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao. Yohane Mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake, wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami.” Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo? Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme. Lakini, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii. “Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu akutangulie, ambaye atakutayarishia njia yako’. Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye. Tangu wakati wa Yohane Mbatizaji mpaka leo hii, ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu. Mafundisho yote ya manabii na sheria mpaka wakati wa Yohane yalibashiri juu ya nyakati hizi. Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Elia ambaye angekuja. Mwenye masikio na asikie! “Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine: ‘Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza! Tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkuomboleza!’ Kwa maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: ‘Amepagawa na pepo’. Mwana wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: ‘Mwangalieni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watozaushuru na wenye dhambi!’ Hata hivyo, hekima ya Mungu inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake.” Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kutubu: “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kujipaka majivu kutubu. Hata hivyo, nawaambieni, siku ya hukumu, nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni. Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo. Lakini nawaambieni, siku ya hukumu wewe utapata adhabu kubwa kuliko ya Sodoma.” Wakati huo Yesu alisema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafunulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza. “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anapenda kumfunulia. Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.” Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake. Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, “Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanya siku ya Sabato.” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao. Au je, hamjasoma katika kitabu cha sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja sheria hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia? Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuu kuliko hekalu. Kama tu mngejua maana ya maneno haya: ‘Nataka huruma wala si tambiko,’ hamngewahukumu watu wasio na hatia. Maana Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.” Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao. Kulikuwa na mtu mmoja mwenye mkono uliopooza. Basi, watu wakamwuliza Yesu, “Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?” Walimwuliza hivyo wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akawaambia, “Tuseme mmoja wenu ana kondoo wake ambaye ametumbukia shimoni; je, hatamshika na kumtoa humo siku ya Sabato? Lakini, mtu ana thamani kuliko kondoo! Basi, ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” Kisha akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukawa mzima kabisa kama ule mwingine. Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu. Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote, akawaamuru wasiwaambie watu habari zake, ili yale aliyosema Mungu kwa njia ya nabii Isaya yatimie: “Tazama mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote. Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale. Kwake yeye mataifa yatakuwa na matumaini.” Hapo watu wakamletea Yesu mtu mmoja kipofu na ambaye alikuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Yesu akamponya hata akaweza kusema na kuona. Umati wote wa watu ulishangaa ukasema, “Je, huenda ikawa huyu ndiye Mwana wa Daudi?” Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, wakasema, “Mtu huyu anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” Yesu, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka. Ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, anajipinga mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamaje? Nyinyi mnasema ati nawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli; je, wafuasi wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo wao ndio watakaowahukumu nyinyi. Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. “Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyanganya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyanganya mali yake. “Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya. Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu. Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao. “Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yatakuwa mazuri; ufanyeni kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya. Mti hujulikana kwa matunda yake. Enyi kizazi cha nyoka! Mnawezaje kusema mambo mema hali nyinyi ni waovu? Maana mtu husema kutokana na yale yaliyojaa moyoni. Mtu mwema hutoa mambo mema katika hazina yake njema; na mtu mbaya hutoa mambo mabaya katika hazina yake mbaya. “Basi, nawaambieni, siku ya hukumu watu watapaswa kujibu juu ya kila neno lisilofaa wanalosema. Maana kwa maneno yako utakubaliwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako utahukumiwa kuwa na hatia.” Kisha baadhi ya waalimu wa sheria na Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.” Naye akawajibu, “Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara, lakini hamtapewa ishara isipokuwa ile ishara ya nabii Yona. Jinsi Yona alivyokaa siku tatu kutwa kucha tumboni mwa nyangumi, ndivyo naye Mwana wa Mtu atakavyokaa ndani ya ardhi siku tatu kutwa kucha. Watu wa Ninewi watatokea wakati wa hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Yona! Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Solomoni. “Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika asipate. Hapo hujisemea: ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka’. Lakini anaporudi na kuikuta tupu, imefagiwa na kupambwa, huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye; na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu.” Yesu alikuwa bado anasema na umati wa watu wakati mama yake na ndugu zake walipofika na kusimama nje, wakitaka kusema naye. Basi, mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kusema nawe.” Lakini Yesu akamjibu mtu huyo, “Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina nani?” Kisha akaunyosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu! Maana yeyote anayefanya atakavyo Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye kaka yangu, dada yangu na mama yangu.” Siku hiyohiyo, Yesu alitoka katika ile nyumba, akaenda na kuketi kando ya ziwa. Makundi makubwa ya watu yalimzunguka hata Yesu akapanda mashuani, akaketi. Watu wote walisimama kwenye ukingo wa ziwa, naye Yesu akawaambia mambo mengi kwa mifano. “Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. Jua lilipochomoza, ziliteketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga. Nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota, zikazaa: Nyingine punje mia, nyingine sitini na nyingine thelathini. Mwenye masikio na asikie!” Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?” Yesu akawajibu, “Nyinyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa. Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. Ndio maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi. Kwao yametimia yale aliyosema nabii Isaya: ‘Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa. Kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameyaziba masikio yao, wameyafumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.’ “Lakini heri yenu nyinyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia. Kweli nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona, wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie. “Basi, nyinyi sikilizeni maana ya mfano huo wa mpanzi. Yeyote asikiaye neno juu ya ufalme wa Mungu bila kuelewa, ni kama zile mbegu zilizoanguka njiani; yule Mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Ile mbegu iliyopandwa penye mawe ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na mara akalipokea kwa furaha. Lakini halishiki na mizizi ndani yake; huendelea kulizingatia neno hilo kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya neno hilo, anakata tamaa mara. Ile mbegu iliyoanguka kati ya miti ya miiba, ni mfano wa mtu asikiaye hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu na anasa za mali hulisonga neno hilo, naye hazai matunda. Ile mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na kuelewa, naye huzaa matunda; mmoja mia, mwingine sitini na mwingine thelathini.” Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja, akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake. Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana. Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, ‘Bwana, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?’ Yeye akawajibu, ‘Adui ndiye aliyefanya hivyo’. Basi, watumishi wake wakamwuliza, ‘Je, unataka twende tukayangoe?’ Naye akawajibu, ‘La, msije labda mnapokusanya magugu, mkangoa na ngano pia. Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: Kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu.’” Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake. Yenyewe ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikisha ota huwa kubwa kuliko mimea yote. Hukua ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake.” Yesu akawaambia mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mama mmoja, akaichanganya na unga madebe mawili na nusu, hata unga wote ukaumuka.” Yesu aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia mifano, ili jambo lililonenwa na nabii litimie: “Nitasema nao kwa mifano; nitafichua yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu.” Kisha Yesu aliwaaga wale watu, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Tufafanulie ule mfano wa magugu shambani.” Yesu akawaambia, “Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni Mwana wa Mtu. Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu. Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika. Kama vile magugu yanavyokusanywa na kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati; Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu, na kuwatupa katika tanuri ya moto, na huko watalia na kusaga meno. Kisha, wale wema watangara kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie! “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri. Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda, akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina. Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: Malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema, na kuwatupa hao wabaya katika tanuri ya moto. Huko watalia na kusaga meno.” Yesu akawauliza, “Je, mmeelewa mambo haya yote?” Wakamjibu, “Naam.” Naye akawaambia, “Hivyo basi, kila mwalimu wa sheria anayekuwa mwanafunzi wa ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.” Yesu alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo, akaenda kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi lao hata wakashangaa, wakasema, “Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu? Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi, amepata wapi haya yote?” Basi, wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi kuheshimiwa, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!” Kwa hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao. Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu. Basi, akawaambia watumishi wake, “Mtu huyu ni Yohane Mbatizaji, amefufuka kutoka kwa wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake.” Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Kisa ni kwamba Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!” Herode alitaka kumuua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii. Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa, hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba. Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, “Nipe papa hapa katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe. Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane. Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake. Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu. Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini. Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao. Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na saa za mchana zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula.” Yesu akawaambia, “Si lazima waende, wapeni nyinyi chakula.” Lakini wao wakamwambia, “Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili.” Yesu akawaambia, “Nileteeni hapa.” Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu. Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ngambo ya ziwa wakati yeye anayaaga makundi ya watu. Baada ya kuwaaga watu, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake, na wakati huo ile mashua ilikwisha fika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikumbwa na taabu kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga. Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji. Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliogopa sana, wakasema, “Ni mzimu!” Wakapiga yowe kwa hofu. Mara, Yesu akasema nao, “Tulieni, ni mimi. Msiogope!” Petro akamwambia, “Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako.” Yesu akasema, “Haya, njoo.” Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu. Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, “Bwana, niokoe!” Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, “Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?” Kisha wakapanda mashuani, na upepo ukatulia. Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.” Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti. Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote, wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake. Nao wote waliomgusa walipona. Kisha Mafarisayo na waalimu wa sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu, wakamwuliza, “Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu? Hawanawi mikono ipasavyo kabla ya kula!” Yesu akawajibu, “Kwa nini nanyi hamjali sheria ya Mungu ila mnapendelea mapokeo yenu wenyewe? Mungu amesema: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima auawe.’ Lakini nyinyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema: ‘Kitu hiki nimemtolea Mungu,’ basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe. Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu: ‘Mungu asema: Watu hawa huniheshimu kwa maneno tu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami. Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’” Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, “Sikilizeni, mkaelewe! Kitu kinachomtia mtu unajisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu unajisi.” Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?” Lakini yeye akawajibu, “Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakupanda, utangolewa. Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni.” Petro akasema, “Tufafanulie huo mfano.” Yesu akasema, “Hata nyinyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutolewa nje chooni? Lakini mambo yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi. Maana moyoni hutoka mawazo ya uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na kashfa. Hayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.” Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni. Basi, mama mmoja Mkanaani wa nchi hiyo alimjia, akapaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo.” Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele.” Yesu akajibu, “Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo.” Hapo huyo mama akaja, akamsujudia, akasema, “Bwana, nisaidie.” Yesu akamjibu, “Si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Huyo mama akajibu, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao.” Hapo Yesu akamjibu, “Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka.” Yule binti yake akapona wakati huohuo. Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi. Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya. Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; watu wakamsifu Mungu wa Israeli. Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende zao bila kula, wasije wakazimia njiani.” Wanafunzi wakamwambia, “Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba na visamaki vichache.” Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu. Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu saba. Hao waliokula walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani. Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni. Lakini Yesu akawajibu, [“Ikifika jioni nyinyi husema: ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu!’ Na alfajiri mwasema: ‘Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu na tena mawingu yametanda!’ Basi, nyinyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia hali ya anga, lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui.] Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ile ya Yona.” Basi, akawaacha, akaenda zake. Wanafunzi wake walipokwisha vukia upande wa pili wa ziwa, walijikuta wamesahau kuchukua mikate. Yesu akawaambia, “Muwe macho na mjihadhari na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!” Lakini wao wakawa wanajadiliana: “Anasema hivyo kwa kuwa hatukuchukua mikate.” Yesu alijua mawazo yao, akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba! Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, hamjaelewa bado? Je, hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale watu 5,000? Je, mlijaza vikapu vingapi vya mabaki? Au, ile mikate saba waliyogawiwa wale watu 4,000, je, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki. Mbona hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!” Hapo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo. Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?” Wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.” Yesu akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Simoni Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Yesu akasema, “Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana hakuna binadamu yeyote aliyekufunulia jambo hili, ila Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia: Wewe ni Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala nguvu za kifo hazitaweza kulishinda. Nitakupa funguo za ufalme wa mbinguni; kila utakachofunga duniani, kitafungwa pia mbinguni; kila utakachofungua duniani, kitafunguliwa pia mbinguni.” Kisha akawaonya wanafunzi wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo. Tangu wakati huo Yesu alianza kuwajulisha waziwazi wanafunzi wake kwamba ni lazima aende Yerusalemu, na huko kupata mateso mengi yatakayosababishwa na wazee, makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Kwamba, atauawa na siku ya tatu atafufuliwa. Hapo Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea: “Isiwe hivyo Bwana! Jambo hili halitakupata!” Lakini Yesu akageuka, akamwambia Petro, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Mawazo yako si ya kimungu ila ni ya kibinadamu!” Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; lakini mtu anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. Je, mtu atafaidi nini akiupata utajiri wote wa ulimwengu na hali amepoteza maisha yake? Au, mtu atatoa kitu gani kiwe badala ya maisha yake? Maana, Mwana wa Mtu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake, na hapo ndipo atakapomlipa kila mtu kadiri ya matendo yake. Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kumwona Mwana wa Mtu akija katika ufalme wake.” Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane nduguye, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao, uso wake ukangaa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama mwanga. Mose na Elia wakawatokea, wakawa wanazungumza naye. Hapo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa! Ukipenda nitajenga vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” Alipokuwa bado anasema hivyo, wingu jeupe likawafunika, na sauti ikasikika kutoka hilo wingu: “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye, msikilizeni.” Wanafunzi waliposikia hivyo wakaanguka kifudifudi, wakaogopa sana. Yesu akawaendea, akawagusa, akasema, “Simameni, msiogope!” Walipoangalia juu hawakumwona mtu, ila Yesu peke yake. Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu akawaonya: “Msimwambie mtu mambo mliyoyaona mpaka Mwana wa Mtu atakapofufuliwa kutoka wafu.” Kisha wanafunzi wakamwuliza, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ni lazima kwanza Elia aje?” Yesu akawajibu, “Kweli, Elia atakuja kutayarisha mambo yote. Lakini nawaambieni, Elia amekwisha kuja nao hawakumtambua, bali walimtendea jinsi walivyotaka. Mwana wa Mtu atateswa vivyo hivyo mikononi mwao.” Hapo hao wanafunzi wakafahamu kwamba alikuwa akiwaambia juu ya Yohane Mbatizaji. Walipoufikia tena ule umati wa watu, mtu mmoja alimwendea Yesu, akampigia magoti, akasema, “Bwana, mwonee huruma mwanangu kwa kuwa ana kifafa, tena anateseka sana; mara nyingi yeye huanguka motoni na majini. Nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumponya.” Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia nyinyi mpaka lini? Mleteni hapa huyo mtoto.” Basi, Yesu akamkemea huyo pepo, naye akamtoka, na yule mtoto akapona wakati huohuo. Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha, wakamwuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa yule pepo?” Yesu akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu haba. Nawaambieni kweli, kama tu mkiwa na imani, iwe ndogo hata kama mbegu ya haradali, mtaweza kuuambia mlima huu: ‘Toka hapa uende pale,’ nao utakwenda. Hakuna chochote ambacho hakingewezekana kwenu. [ Pepo wa namna hii hawezi kuondolewa ila kwa sala na kufunga.”] Walipokuwa pamoja huko Galilaya, Yesu aliwaambia, “Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu. Watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa.” Wanafunzi wakahuzunika mno. Walipofika Kafarnaumu watu wenye kukusanya fedha ya zaka ya hekalu walimwendea Petro, wakamwuliza, “Je, mwalimu wenu hulipa fedha ya zaka?” Petro akajibu, “Naam, hulipa.” Basi, Petro alipoingia ndani ya nyumba, kabla hata hajasema neno, Yesu akamwuliza, “Simoni, wewe unaonaje? Wafalme wa dunia hukusanya ushuru au kodi kutoka kwa kina nani? Kutoka kwa wananchi ama kutoka kwa wageni?” Petro akajibu, “Kutoka kwa wageni.” Yesu akamwambia, “Haya basi, wananchi hawahusiki. Lakini kusudi tusiwakwaze, nenda ziwani ukatupe ndoana; chukua samaki wa kwanza atakayenaswa, fungua kinywa chake, na ndani utakuta fedha taslimu ya zaka. Ichukue ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.” Wakati ule wanafunzi walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Ni nani aliye mkubwa zaidi katika ufalme wa mbinguni?” Yesu akamwita mtoto mmoja, akamsimamisha kati yao, kisha akasema, “Nawaambieni kweli, msipogeuka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Yeyote anayejinyenyekesha kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Yeyote anayempokea mtoto mmoja kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi. “Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari. Ole wake ulimwengu kwa sababu ya vikwazo vinavyowaangusha wengine. Vikwazo hivyo ni lazima vitokee lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha. “Kama mkono au mguu wako ukikukosesha, ukate na kuutupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai bila mkono au mguu, kuliko kutupwa katika moto wa milele ukiwa na mikono miwili na miguu yako miwili. Na jicho lako likikukosesha, lingoe na kulitupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai ukiwa chongo, kuliko kutupwa katika moto wa Jehanamu ukiwa na macho yako yote mawili. “Jihadharini! Msimdharau mmojawapo wa wadogo hawa. Nawaambieni, malaika wao huko mbinguni wako daima mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. [ Maana Mwana wa Mtu alikuja kuwaokoa wale waliopotea.] (Taz Luka 19:10). Mnaonaje? Mtu akiwa na kondoo 100, akimpoteza mmoja, hufanyaje? Huwaacha wale tisini na tisa mlimani, akaenda kumtafuta yule aliyepotea. Akimpata, nawaambieni kweli, humfurahia huyo kuliko awafurahiavyo wale tisini na tisa ambao hawakupotea. Hali kadhalika, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmoja wa hawa wadogo apotee. “Ndugu yako akikukosea, mwendee ukamwonye mkiwa nyinyi peke yenu. Akikusikia utakuwa umempata ndugu yako. Asipokusikia, chukua mtu mmoja au wawili pamoja nawe, ili kwa mawaidha ya mashahidi wawili au watatu, kila tatizo litatuliwe. Asipowasikia hao, liambie kanisa. Na kama hatalisikia kanisa, na awe kwako kama watu wasiomjua Mungu na watozaushuru. “Nawaambieni kweli, mtakachofunga duniani kitafungwa mbinguni, na mtakachofungua duniani kitafunguliwa mbinguni. Tena nawaambieni, wawili miongoni mwenu wakikubaliana hapa duniani kuhusu jambo lolote la kuomba, Baba yangu wa mbinguni atawafanyia jambo hilo. Kwa maana popote pale wanapokusanyika wawili au watatu kwa jina langu, mimi nipo hapo kati yao.” Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, “Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?” Yesu akamjibu, “Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba. Ndiyo maana ufalme wa mbinguni unafanana na mfalme mmoja aliyeamua kukagua hesabu za watumishi wake. Ukaguzi ulipoanza, akaletewa mtu mmoja aliyekuwa na deni la fedha talanta 10,000. Mtu huyo hakuwa na chochote cha kulipa; hivyo bwana wake aliamuru auzwe, yeye, mke wake, watoto wake na vitu vyote alivyokuwa navyo, ili deni lilipwe. Basi, huyo mtumishi akapiga magoti mbele yake, akasema, ‘Unisubiri nami nitakulipa deni lote’. Yule bwana alimwonea huruma, akamsamehe lile deni, akamwacha aende zake. “Lakini huyo mtumishi akaondoka, akamkuta mmoja wa watumishi wenzake aliyekuwa na deni lake fedha dinari 100. Akamkamata, akamkaba koo akisema, ‘Lipa deni lako!’ Huyo mtumishi mwenzake akapiga magoti, akamwomba, ‘Unisubiri nami nitakulipa’. Lakini yeye hakutaka, bali alimtia gerezani mpaka hapo atakapolipa lile deni. “Basi, watumishi wenzake walipoona jambo hilo walisikitika sana, wakaenda kumpasha habari bwana wao juu ya mambo hayo yaliyotukia. Hapo yule bwana alimwita huyo mtumishi, akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mbaya sana! Uliniomba, nami nikakusamehe deni lako lote. Je, haikukupasa nawe kumhurumia mtumishi mwenzako kama nilivyokuhurumia?’ “Basi, huyo bwana alikasirika sana, akamtoa huyo mtumishi aadhibiwe mpaka hapo atakapolipa deni lote. Na baba yangu aliye mbinguni atawafanyieni vivyo hivyo kama kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kwa moyo wake wote.” Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, alitoka Galilaya, akaenda Yudea, ngambo ya mto Yordani. Watu wengi walimfuata huko, naye akawaponya. Mafarisayo kadhaa walimjia, wakamwuliza kwa kumtega, “Je, ni halali mume kumpa talaka mkewe kwa kisa chochote?” Yesu akawajibu, “Je, hamkusoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Mungu aliyemuumba mtu tangu mwanzo alimfanya mwanamume na mwanamke, na akasema: ‘Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja?’ Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja. Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asikitenganishe.” Lakini wao wakamwuliza, “Kwa nini basi, Mose alituagiza mwanamke apewe hati ya talaka na kuachwa?” Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo. Basi nawaambieni, yeyote atakayemwacha mke wake isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, akaoa mke mwingine, anazini.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Ikiwa mambo ya mume na mkewe ni hivyo, ni afadhali kutooa kabisa.” Yesu akawaambia, “Si wote wanaoweza kulipokea fundisho hili, isipokuwa tu wale waliojaliwa na Mungu. Maana kuna sababu kadhaa za kutoweza kuoa: Wengine ni kwa sababu wamezaliwa hivyo, wengine kwa sababu wamefanywa hivyo na watu, na wengine wameamua kutooa kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee.” Kisha watu wakamletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi wakawakemea. Yesu akasema, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie; maana ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto hawa.” Basi, akawawekea mikono, kisha akaondoka mahali hapo. Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, “Mwalimu, nifanye kitu gani chema ili niupate uhai wa milele?” Yesu akamwambia, “Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uhai, shika amri.” Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?” Yesu akasema, “Usiue, Usizini, Usiibe, Usitoe ushahidi wa uongo, Waheshimu baba yako na mama yako; na, Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Huyo kijana akamwambia, “Hayo yote nimeyazingatia; nifanye nini zaidi?” Yesu akamwambia, “Kama unapenda kuwa mkamilifu, nenda ukauze mali yako, uwape maskini fedha hiyo, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate.” Huyo kijana aliposikia hayo, akaenda zake akiwa mwenye huzuni, maana alikuwa na mali nyingi. Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kweli nawaambieni itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Wale wanafunzi waliposikia hivyo walishangaa sana, wakamwuliza, “Ni nani basi, awezaye kuokoka?” Yesu akawatazama, akasema, “Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana.” Kisha Petro akasema, “Na sisi je? Tumeacha yote tukakufuata; tutapata nini basi?” Yesu akawaambia, “Nawaambieni kweli, Mwana wa Mtu atakapoketi katika kiti chake cha enzi kitukufu katika ulimwengu mpya, nyinyi mlionifuata mtaketi katika viti kumi na viwili mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. Na kila aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi, na kupata uhai wa milele. Lakini walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza. “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake. Akapatana nao kuwalipa fedha denari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi. Akawaambia, ‘Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.’ Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo. Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, ‘Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?’ Wakamjibu: ‘Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.’ Naye akawaambia, ‘Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.’ “Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, ‘Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.’ Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja fedha dinari moja. Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja. Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnungunikia yule bwana. Wakasema, ‘Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?’ “Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa dinari moja? Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?’” Yesu akamaliza kwa kusema, “Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho.” Yesu alipokuwa anakwenda juu Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia, “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waalimu wa sheria, nao watamhukumu auawe. Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa.” Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu. Yesu akamwuliza, “Unataka nini?” Huyo mama akamwambia, “Ahidi kwamba katika ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto.” Yesu akajibu, “Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?” Wakamjibu, “Tunaweza.” Yesu akawaambia, “Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu.” Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili. Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao. Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote; na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu. Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.” Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata. Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!” Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!” Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakamjibu, “Bwana, tunaomba macho yetu yafumbuliwe.” Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata. Yesu na wanafunzi wake walipokaribia Yerusalemu na kufika Bethfage katika mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, “Nendeni hadi kijiji kilicho mbele yenu na mtamkuta punda amefungwa na mtoto wake. Wafungueni mkawalete kwangu. Kama mtu akiwauliza sababu, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji,’ naye atawaachieni mara.” Jambo hili lilifanyika ili yale yaliyosemwa na nabii yatimie: “Uambieni mji wa Siyoni: Tazama, Mfalme wako anakujia! Ni mpole na amepanda punda, mwanapunda, mtoto wa punda.” Hivyo, wale wanafunzi walikwenda wakafanya kama Yesu alivyowaagiza. Wakamleta yule punda na mtoto wake, wakatandika nguo zao juu yao na Yesu akaketi juu yake. Umati mkubwa wa watu wakatandaza nguo zao barabarani, na watu wengine wakakata matawi ya miti wakayatandaza barabarani. Makundi ya watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti: “Sifa kwa Mwana wa Daudi! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Sifa kwa Mungu juu!” Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawa wanauliza, “Huyu ni nani?” Watu katika ule umati wakasema, “Huyu ni nabii Yesu, kutoka Nazareti mji wa Galilaya.” Basi, Yesu akaingia hekaluni, akawafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu ndani ya hekalu; akazipindua meza za wale waliokuwa wanavunja fedha, na viti vya wale waliokuwa wanauza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala.’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi.” Vipofu na vilema wengine walimwendea huko hekaluni, naye Yesu akawaponya. Basi, makuhani wakuu na waalimu wa sheria walipoyaona maajabu aliyoyafanya Yesu, na pia watoto walipokuwa wanapaza sauti zao hekaluni wakisema: “Sifa kwa Mwana wa Daudi,” wakakasirika. Hivyo wakamwambia, “Je, husikii wanachosema?” Yesu akawajibu, “Naam, nasikia! Je hamjapata kusoma Maandiko haya? ‘Kwa vinywa vya watoto wadogo na wachanga wajipatia sifa kamili.’” Basi, akawaacha, akatoka nje ya mji na kwenda Bethania, akalala huko. Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa. Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauna chochote ila majani matupu. Basi, akauambia, “Usizae tena matunda milele!” Papo hapo huo mtini ukanyauka. Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, “Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?” Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ itafanyika hivyo. Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba kwa sala, mtapata.” Yesu aliingia hekaluni, akawa anafundisha. Alipokuwa akifundisha, makuhani wakuu na wazee wa watu wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani amekupa mamlaka haya?” Yesu akawajibu, “Na mimi nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, basi nami nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa nani? Je, yalitoka mbinguni ama kwa watu?” Lakini wakajadiliana wao kwa wao hivi: “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’ Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu,’ tunaogopa umati wa watu maana wote wanakubali kwamba Yohane ni nabii.” Basi, wakamjibu, “Hatujui!” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. “Nyinyi mnaonaje; mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwambia yule wa kwanza, ‘Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.’ Yule kijana akamwambia, ‘Sitaki!’ Lakini baadaye akabadili nia, akaenda kufanya kazi. Yule baba akamwambia mtoto wake wa pili vivyo hivyo, naye akamjibu, ‘Naam baba!’ Lakini hakuenda kazini. Je, ni nani kati ya hawa wawili aliyetimiza matakwa ya baba yake?” Wakamjibu, “Yule mtoto wa kwanza.” Basi, Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, watozaushuru na waasherati wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu. Maana Yohane alikuja kwenu akawaonesha njia adili ya kuishi, nanyi hamkumwamini; lakini watozaushuru na waasherati walimwamini. Hata baada ya kuona hayo yote nyinyi hamkutubu na kumsadiki.” Yesu akasema, “Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda hadi nchi ya mbali. Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake. Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamuua na mwingine wakampiga mawe. Huyo mtu akawatuma tena watumishi wengine, wengi kuliko wa safari ya kwanza. Wale wakulima wakawatendea namna ileile. Mwishowe akamtuma mwanawe huku akifikiri: ‘Watamjali mwanangu.’ Lakini wale wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: ‘Huyu ndiye mrithi; na tumuue ili tuuchukue urithi wake!’ Basi, wakamkamata, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua. “Sasa, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyaje hao wakulima?” Wao wakamjibu, “Atawaangamiza vibaya hao waovu, na lile shamba atawapa wakulima wengine ambao watampa sehemu ya mavuno wakati wake.” Hapo Yesu akawaambia, “Je, hamkusoma jambo hili katika Maandiko Matakatifu? ‘Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi. Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu!’ “Kwa hiyo nawaambieni, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wa mataifa mengine wenye kutoa matunda yake.” Atakayeanguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda” (taz. Luka 20:18). Makuhani wakuu na Mafarisayo waliposikia hiyo mifano yake walitambua kwamba alikuwa anawasema wao. Kwa hiyo wakawa wanatafuta njia ya kumtia nguvuni, lakini waliwaogopa watu kwa sababu wao walimtambua yeye kuwa nabii. Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano: “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya harusi. Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje harusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika. Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa: Karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ndama wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari; njoni harusini.’ Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake, na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua. Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumishi wake: ‘Karamu ya harusi iko tayari kweli, lakini walioalikwa hawakustahili. Basi, nendeni kwenye barabara na wowote wale mtakaowakuta waiteni waje harusini.’ Wale watumishi wakatoka, wakaenda njiani, wakawaleta watu wote, wabaya na wema. Nyumba ya harusi ikajaa wageni. “Mfalme alipoingia kuwaona wageni, akamwona mtu mmoja ambaye hakuvaa mavazi ya harusi. Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la harusi?’ Lakini yeye akakaa kimya. Hapo mfalme akawaambia watumishi, ‘Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno.’” Yesu akamaliza kwa kusema, “Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa.” Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake. Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako. Haya, tuambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari?” Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, “Enyi wanafiki mbona mnanijaribu? Nionesheni fedha ya kulipia kodi.” Nao wakamtolea sarafu ya fedha. Basi, Yesu akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Hapo Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao. Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo wasemao wafu hawafufuki walimwendea Yesu. Basi, wakamwambia, “Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto. Basi, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane. Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba. Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama. Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.” Yesu akawajibu, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika mbinguni. Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, je, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? Aliwaambia, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo!’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake. Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, wakakutana pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza Yesu kwa kumjaribu, “Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika sheria?” Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote’. Hii ndiyo amri kuu na ya kwanza. Ya pili inafanana na hiyo: ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe’. Sheria yote ya Mose na mafundisho ya manabii vinategemea amri hizi mbili.” Mafarisayo walipokusanyika pamoja, Yesu aliwauliza, “Nyinyi mwaonaje juu ya Kristo? Je, ni mwana wa nani?” Wakamjibu, “Wa Daudi.” Yesu akawaambia, “Basi, inawezekanaje kwamba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Daudi anamwita yeye Bwana? Maana alisema: ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke maadui zako chini ya miguu yako.’ Basi, ikiwa Daudi anamwita Kristo ‘Bwana,’ anawezaje kuwa mwanawe?” Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumjibu neno. Na tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu tena kumwuliza swali. Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, “Waalimu wa sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kufafanua sheria ya Mose. Kwa hiyo shikeni na kutekeleza chochote watakachowaambieni. Lakini msiyaige matendo yao, maana hawatekelezi yale wanayoyahubiri. Hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, lakini wao wenyewe hawataki kunyosha hata kidole wapate kuibeba. Wao hufanya matendo yao yote ili watu wawaone. Huvaa tepe zenye maandishi ya sheria juu ya panda la uso na mikononi na hupanua pindo za makoti yao. Hupenda nafasi za heshima katika karamu na viti vya heshima katika masunagogi. Hupenda kusalimiwa kwa heshima sokoni na kupendelea kuitwa na watu: ‘Mwalimu.’ Lakini nyinyi msiitwe kamwe ‘Mwalimu,’ maana mwalimu wenu ni mmoja tu, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu yeyote ‘Baba’ hapa duniani, maana Baba yenu ni mmoja tu, aliye mbinguni. Wala msiitwe ‘Viongozi,’ maana kiongozi wenu ni mmoja tu, ndiye Kristo. Aliye mkubwa miongoni mwenu ni lazima awe mtumishi wenu. Anayejikweza atashushwa, na anayejishusha atakwezwa. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnaufunga mlango wa ufalme wa mbinguni mbele ya macho ya watu. Nyinyi wenyewe hamwingii ndani, wala hamwaruhusu wanaotaka kuingia waingie. [ Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnawanyonya wajane na kujisingizia kuwa watu wema kwa kusali sala ndefu. Kwa sababu hiyo mtapata adhabu kali.] (Taz Marko 12:40). “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumpata mtu mmoja afuate dini yenu. Mnapompata, mnamfanya astahili maradufu kwenda katika moto wa Jehanamu kuliko nyinyi wenyewe. “Ole wenu viongozi vipofu! Nyinyi mwasema ati mtu akiapa kwa hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini akiapa kwa dhahabu ya hekalu, kiapo hicho kinamshika. Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: Dhahabu au hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu? Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika. Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: Ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu? Anayeapa kwa madhabahu ameapa kwa hiyo madhabahu, na kwa chochote kilichowekwa juu yake. Na anayeapa kwa hekalu ameapa kwa hilo hekalu na pia kwa yule akaaye ndani yake. Na anayeapa kwa mbingu ameapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa huyo aketiye juu yake. Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu sehemu moja ya kumi, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndio hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine. Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia! “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyanganyi na uchoyo. Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu. Hali kadhalika nyinyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya watu wema. Mwasema: ‘Kama sisi tungaliishi nyakati za wazee wetu hatungalishirikiana nao katika mauaji ya manabii!’ Hivyo mnathibitisha nyinyi wenyewe kwamba nyinyi ni watoto wa watu waliowaua manabii. Haya, kamilisheni ile kazi wazee wenu waliyoianza! Enyi kizazi cha nyoka wenye sumu! Mnawezaje kuiepa hukumu ya moto wa Jehanamu? Ndio maana mimi ninawapelekea nyinyi manabii, watu wenye hekima na waalimu; mtawaua na kuwasulubisha baadhi yao, na wengine mtawapiga viboko katika masunagogi yenu na kuwasaka katika kila mji. Hivyo lawama yote itawapateni kwa ajili ya damu yote ya watu wema iliyomwagwa juu ya ardhi. Naam, tangu kumwagwa damu ya Abeli ambaye hakuwa na hatia, mpaka ile ya Zakaria, mwana wa Barakia, ambaye mlimuua hekaluni kati ya patakatifu na madhabahu. Nawaambieni kweli, kizazi hiki kitapata adhabu kwa sababu ya mambo haya. “Yerusalemu! Ee Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako. Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya watoto wako kwangu, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka. Haya basi, nyumba yako itaachwa mahame. Nakuambia, hutaniona tena mpaka wakati utakaposema: ‘Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.’” Yesu alitoka hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea, wakamwonesha majengo ya hekalu. Yesu akawaambia, “Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa.” Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani, wakamwuliza, “Tuambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?” Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. Maana wengi watatokea wakisema kila mmoja kwamba yeye ndiye Kristo nao watawapotosha watu wengi. Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado. Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi. Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto. “Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa sababu ya jina langu. Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana. Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi. Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa. Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote. “Basi, mtakapoona ‘Chukizo Haribifu lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake), hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani. Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake. Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato! Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena. Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa. “Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: ‘Kristo yuko hapa’ au ‘Yuko pale,’ msimsadiki. Maana watatokea akina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu. Sikilizeni, nimekwisha waonya kabla ya wakati. Basi, wakiwaambieni, ‘Tazameni, yuko jangwani,’ msiende huko; au, ‘Tazameni, amejificha ndani,’ msisadiki; maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai. “Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi. Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu. “Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa mavuno umekaribia. Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana. Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. “Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina. Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja. Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu. Lakini kumbukeni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.” Yesu akaendelea kusema, “Ni nani basi mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape chakula kwa wakati wake? Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo. Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali yake yote. Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: ‘Bwana wangu amekawia kurudi,’ kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula na kunywa pamoja na walevi, bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua. Atamwadhibu vibaya na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno. “Wakati huo, ufalme wa mbinguni utafanana na wasichana kumi waliochukua taa zao, wakaenda kumlaki bwana arusi. Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara. Wale wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta. Lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao. Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wasichana wote walisinzia, wakalala. Usiku wa manane kukawa na kelele: ‘Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.’ Hapo wale wasichana wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao. Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: ‘Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa zetu zinazimika.’ Lakini wale wenye busara wakawaambia, ‘Hayatatutosha sisi na nyinyi! Afadhali mwende dukani mkajinunulie wenyewe!’ Basi, wale wasichana wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na wale wasichana waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la harusi, kisha mlango ukafungwa. Baadaye wale wasichana wengine wakaja, wakaita: ‘Bwana, Bwana, tufungulie!’ Lakini yeye akawajibu, ‘Nawaambieni kweli, siwajui nyinyi.’” Kisha Yesu akasema, “Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa. “Wakati huo itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ngambo: Aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake. Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: Mmoja fedha talanta tano, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri. Mara yule aliyekabidhiwa fedha talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano. Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili. Lakini yule aliyekabidhiwa fedha talanta moja akaenda, akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake. “Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake. Mtumishi aliyekabidhiwa fedha talanta tano akaja amechukua talanta tano faida, akamwambia, ‘Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi faida niliyopata.’ Bwana wake akamwambia, ‘Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’ “Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida, akisema, ‘Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.’ Bwana wake akamwambia, ‘Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’ “Lakini yule aliyekabidhiwa fedha talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya. Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.’ “Bwana wake akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya. Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake! Basi, mnyanganyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi. Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. Na kuhusu huyu mtumishi asiye na faida, mtupeni nje gizani! Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’ “Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu. Mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi. Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto. “Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, ‘Njoni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha; nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.’ Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme ‘Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji? Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika? Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?’ Mfalme atawajibu, ‘Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.’ “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake. Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji. Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama.’ “Hapo nao watajibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, ukiwa mgeni au bila nguo, ukiwa mgonjwa au mfungwa, nasi hatukukuhudumia?’ Naye atawajibu, ‘Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.’ Basi, hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uhai wa milele.” Yesu alipomaliza kusema hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake, “Mnajua kwamba baada ya siku mbili tutakuwa na sikukuu ya Pasaka, na Mwana wa Mtu atatolewa ili asulubiwe.” Wakati huo makuhani wakuu na wazee wa watu walikutana pamoja katika ukumbi wa Kayafa, kuhani mkuu. Wakashauriana jinsi ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue. Lakini wakaamua jambo hilo lisifanyike wakati wa sikukuu, kusije kukatokea ghasia kati ya watu. Yesu alipokuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, aitwaye Mkoma, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya thamani kubwa, alimjia pale mezani alipokuwa amekaa kula chakula, akammiminia hayo marashi kichwani. Wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Ya nini hasara hii? Marashi haya yangaliweza kuuzwa kwa bei kubwa, maskini wakapewa hizo fedha.” Yesu alitambua mawazo yao, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mama? Yeye amenitendea jambo jema. Maskini mnao daima pamoja nanyi, lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima. Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko. Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni ambapo hii Habari Njema itahubiriwa, kitendo hiki alichofanya mama huyu kitatajwa kwa kumkumbuka yeye.” Kisha, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, akaenda kwa makuhani wakuu, akawaambia, “Mtanipa kitu gani kama nikimkabidhi Yesu kwenu?” Wakamhesabia vipande thelathini vya fedha; na tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta nafasi ya kumsaliti. Siku ya kwanza kabla ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi walimwendea Yesu wakamwuliza, “Unataka tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?” Yeye akawajibu, “Nendeni mjini kwa mwanamume fulani, mkamwambie: ‘Mwalimu anasema, wakati wangu umefika; kwako nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.’” Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaandaa Pasaka. Kulipokuwa jioni, Yesu akakaa mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Nawaambieni kweli, mmoja wenu atanisaliti.” Wanafunzi wakahuzunika sana, wakaanza kuuliza mmojammoja, “Bwana! Je, ni mimi?” Yesu akajibu, “Anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli ndiye atakayenisaliti. Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo, lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa.” Yuda, ambaye ndiye aliyetaka kumsaliti, akamwuliza, “Mwalimu! Je, ni mimi?” Yesu akamjibu, “Wewe umesema.” Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, “Kunyweni nyote; maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi. Nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.” Baada ya kuimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni. Kisha Yesu akawaambia, “Usiku huu wa leo, nyinyi nyote mtakuwa na mashaka nami, maana Maandiko Matakatifu yasema: ‘Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.’ Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulieni Galilaya.” Petro akamwambia Yesu, “Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakuacha kamwe.” Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Petro akamwambia, “Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Wale wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo. Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali.” Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko. Hapo akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.” Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe.” Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Ndio kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.” Akaenda tena mara ya pili akasali: “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kipite bila mimi kukinywa, basi, utakalo lifanyike.” Akawaendea tena, akawakuta wamelala, maana macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale. Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia, “Je, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi. Amkeni; twendeni zetu. Tazameni! Anakuja yule atakayenisaliti.” Basi, Yesu alipokuwa bado anasema nao, mara akaja Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili. Pamoja naye walikuja watu wengi wenye mapanga na marungu ambao walitumwa na makuhani wakuu na wazee wa watu. Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha kuwapa ishara akisema: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni.” Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, “Shikamoo, Mwalimu!” Kisha akambusu. Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya ulichokuja kufanya.” Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. Mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Hapo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako alani, maana yeyote anayeutumia upanga, atakufa kwa upanga. Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya vikosi kumi na viwili vya malaika? Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?” Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, “Je, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Kila siku nilikuwa hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata! Lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie.” Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Basi, hao watu waliomkamata Yesu walimpeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu, walikokusanyika waalimu wa sheria na wazee. Petro alimfuata kwa mbali mpaka uani kwa kuhani mkuu, akaingia ndani pamoja na walinzi ili apate kuona mambo yatakavyokuwa. Basi, makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu wapate kumuua, lakini hawakupata ushahidi wowote, ingawa walikuja mashahidi wengi wa uongo. Mwishowe wakaja mashahidi wawili, wakasema, “Mtu huyu alisema: ‘Ninaweza kuliharibu hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’” Kuhani mkuu akasimama, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?” Lakini Yesu akakaa kimya. Kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu!” Yesu akamwambia, “Wewe umesema! Lakini nawaambieni, tangu sasa mtamwona Mwana wa Mtu ameketi upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.” Hapo, kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi? Sasa mmesikia kufuru yake. Nyinyi mwaonaje?” Wao wakamjibu, “Anastahili kufa!” Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makofi. Wengine wakiwa wanampiga makofi, wakasema, “Tubashirie basi, wewe Kristo; ni nani amekupiga!” Petro alikuwa ameketi nje uani. Basi, mtumishi mmoja wa kike akamwendea, akasema, “Wewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.” Petro akakana mbele ya wote akisema, “Sijui hata unasema nini.” Alipokuwa akitoka mlangoni, mtumishi mwingine wa kike akamwona, akawaambia wale waliokuwa pale, “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.” Petro akakana tena kwa kiapo: “Simjui mtu huyo.” Baadaye kidogo, watu waliokuwa pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika, wewe pia ni mmoja wao, maana msemo wako unakutambulisha.” Hapo Petro akaanza kujilaani na kuapa akisema, “Simjui mtu huyo!” Mara jogoo akawika. Petro akakumbuka maneno aliyoambiwa na Yesu: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Basi, akatoka nje, akalia sana. Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumuua. Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa. Hapo, Yuda, ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu vile vipande thelathini vya fedha. Akawaambia, “Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe.” Lakini wao wakasema, “Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako.” Naye akazitupa zile fedha hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga. Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, “Haifai kuziweka katika hazina ya hekalu kwa maana ni fedha za damu.” Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. Ndio maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu. Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: “Walichukua vipande thelathini vya fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walimtia bei, wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.” Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, “Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamwambia, “Wewe umesema.” Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno. Hivyo Pilato akamwuliza, “Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?” Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana. Ilikuwa kawaida wakati wa sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka. Wakati huo kulikuwa na mfungwa aliyejulikana sana, jina lake Baraba. Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, “Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba ama Yesu aitwaye Kristo?” Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu. Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: “Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.” Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe. Mkuu wa mkoa akawauliza, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?” Wakamjibu, “Baraba!” Pilato akawauliza, “Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?” Wote wakasema, “Asulubiwe!” Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya ubaya gani?” Wao wakazidi kupaza sauti: “Asulubiwe!” Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe.” Watu wote wakasema, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!” Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa asulubiwe. Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu. Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, “Shikamoo mfalme wa Wayahudi!” Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani. Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha. Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu. Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa, wakampa mchanganyiko wa divai na kitu kichungu. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa. Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. Wakaketi, wakawa wanamchunga. Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lililoandikwa, “Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.” Wanyanganyi wawili walisulubiwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia. Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Wewe! Si ulijidai kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi, shuka msalabani!” Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria na wazee walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Ati yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini. Alimtumainia Mungu na kusema ati yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka.” Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana. Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, giza likaikumba nchi yote. Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, “Eli, Eli, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, “Anamwita Elia.” Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe. Wengine wakasema, “Acha tuone kama Elia anakuja kumwokoa.” Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho. Hapo pazia la hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa; nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika mji mtakatifu, wakaonekana na watu wengi. Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Arimathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe. Yosefu akauchukua ule mwili, akauzungushia sanda safi ya kitani, akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake. Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi. Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato, Wakasema, “Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya zaidi kuliko ule wa awali.” Pilato akawaambia, “Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo.” Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi. Baada ya Sabato, karibu na mapambazuko ya siku ile ya Jumapili, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile kaburi. Ghafla kukatokea tetemeko kubwa la nchi; malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akalivingirisha lile jiwe, akalikalia. Alionekana kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. Walinzi wa lile kaburi wakatetemeka kwa hofu kubwa, hata wakawa kama wamekufa. Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, “Nyinyi msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa maana amefufuka kama alivyosema. Njoni mkaone mahali alipokuwa amelala. Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba amefufuka kutoka kwa wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona. Haya, mimi nimekwisha waambieni.” Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake. Mara, Yesu akakutana nao, akasema: “Salamu.” Hao wanawake wakamwendea, wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake. Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, na huko wataniona.” Wale wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia. Basi, wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha wakisema, “Nyinyi mtasema hivi: ‘Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tukiwa tumelala.’ Na kama mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa nyinyi hamtapata matatizo.” Wale walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo. Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya kwenye ule mlima aliowaagizia Yesu. Walipomwona wakamwabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka. Yesu akaja karibu, akawaambia, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati.” Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Mungu alisema, ‘Namtuma mjumbe wangu akutangulie, ambaye atakutayarishia njia yako.’ Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake, nyosheni barabara zake.’” Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao. Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Naye alihubiri akisema, “Baada yangu anakuja mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.” Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani. Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.” Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani, akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamhudumia. Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!” Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu. Yesu akawaambia, “Nifuateni nami nitawafanya nyinyi kuwa wavuvi wa watu.” Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata. Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika sunagogi, akaanza kufundisha. Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama waalimu wao wa sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka. Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu, akapaza sauti, “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!” Yesu akamkemea huyo pepo akisema, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu.” Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka. Watu wote wakashangaa, wakaulizana, “Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika eneo la Galilaya. Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao. Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili. Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia. Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo. Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango. Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani. Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda mahali pa faragha kusali. Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta. Walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta.” Yesu akawaambia, “Twendeni katika miji mingine ya jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo.” Basi, akaenda kila mahali huko Galilaya akihubiri katika masunagogi na kufukuza pepo. Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba: “Ukitaka, waweza kunitakasa!” Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, “Nataka! Takasika!” Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika. Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwambia, “Angalia usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani na ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.” Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande. Baada ya siku kadhaa, Yesu alirudi Kafarnaumu, watu wakapata habari kwamba alikuwa nyumbani. Basi, wakaja watu wengi sana hata nafasi yoyote ikakosekana mlangoni. Yesu alikuwa akiwahubiria ujumbe wake, wakati mtu mmoja aliyepooza alipoletwa kwake akiwa amechukuliwa na watu wanne. Kwa sababu ya huo umati wa watu, hawakuweza kumpeleka karibu na Yesu. Basi, wakatoboa sehemu ya paa iliyokuwa juu ya mahali alipokuwa Yesu. Walipokwisha pata nafasi, wakamteremsha huyo mtu akiwa amelala juu ya mkeka. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.” Baadhi ya waalimu wa sheria waliokuwa wameketi hapo wakawaza mioyoni mwao, “Anathubutuje kusema hivyo? Anamkufuru Mungu! Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake.” Yesu alitambua mara mawazo yao, akawaambia, “Mbona mnawaza hivyo mioyoni mwenu? Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kumwambia, ‘Inuka! Chukua mkeka wako utembee?’ Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anayo mamlaka ya kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Nakuambia simama; chukua mkeka wako uende nyumbani!” Mara, watu wote wakiwa wanamtazama, huyo mtu akainuka, akauchukua mkeka wake, akaenda zake. Watu wote wakashangaa na kumtukuza Mungu wakisema, “Hatujapata kamwe kuona jambo kama hili.” Yesu alikwenda tena kando ya ziwa. Umati wa watu ukamwendea, naye akaanza kuwafundisha. Alipokuwa akipita, akamwona Lawi mwana wa Alfayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Lawi akasimama, akamfuata. Baadaye, Yesu alikuwa amekaa mezani, nyumbani kwa Lawi, kula chakula. Watozaushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wamemfuata Yesu na wengi wao wakawa wamekaa mezani pamoja naye na wanafunzi wake. Basi, baadhi ya waalimu wa sheria ambao walikuwa Mafarisayo walipomwona Yesu akila pamoja na watu wenye dhambi na watozaushuru, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini anakula pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?” Yesu alipowasikia, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, ila wenye dhambi.” Wakati mmoja wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo walikuwa wanafunga. Basi, watu wakaja, wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wa Yohane na wa Mafarisayo wanafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akajibu, “Je, walioalikwa harusini hutakiwa kufunga wakati bwana arusi yupo pamoja nao? Wakati wote wawapo pamoja na bwana arusi hawawezi kufunga. Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga. “Watu hawakati kiraka cha nguo mpya na kukishonea katika nguo kuukuu. Kama wakifanya hivyo, hicho kiraka kipya kitararuka kutoka hilo vazi kuukuu, nalo litaharibika zaidi. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu. Kama wakifanya hivyo, divai itavipasua hivyo viriba, nayo divai pamoja na hivyo viriba vitaharibika. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya!” Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano. Walipokuwa wanatembea, wanafunzi wake wakaanza kukata masuke ya ngano. Mafarisayo wakawaambia, “Tazama! Kwa nini wanafanya jambo ambalo si halali kufanya siku ya Sabato?” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Yeye aliingia ndani ya Nyumba ya Mungu, akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Jambo hili lilifanyika wakati Abiathari alikuwa kuhani mkuu. Na ni makuhani tu peke yao waliokuwa wameruhusiwa kula mikate hiyo. Lakini Daudi aliila, tena akawapa na wenzake.” Basi, Yesu akawaambia, “Sabato iliwekwa kwa ajili ya binadamu na si binadamu kwa ajili ya Sabato! Kwa hiyo, Mwana wa Mtu ana uwezo hata juu ya Sabato.” Yesu aliingia tena katika sunagogi na mle ndani mlikuwa na mtu aliyekuwa na mkono uliopooza. Humo, baadhi ya watu walimngojea amponye mtu huyo siku ya Sabato ili wapate kumshtaki. Yesu akamwambia huyo mtu aliyekuwa na mkono uliopooza, “Njoo hapa katikati.” Kisha, akawauliza, “Je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao hawakusema neno. Hapo akawatazama wote kwa hasira, akaona huzuni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Kisha akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako!” Naye akaunyosha mkono wake, ukawa mzima tena. Mara Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri pamoja na watu wa kikundi cha Herode jinsi ya kumwangamiza Yesu. Yesu aliondoka hapo pamoja na wanafunzi wake, akaenda kando ya ziwa, na umati wa watu ukamfuata. Watu hao walikuwa wametoka Yerusalemu, Yudea, Idumea, ngambo ya mto Yordani, Tiro na Sidoni. Watu hao wengi walimwendea Yesu kwa sababu ya kusikia mambo mengi aliyokuwa ameyatenda. Yesu akawaambia wanafunzi wake wamtayarishie mashua moja, ili umati wa watu usije ukamsonga. Alikuwa amewaponya watu wengi, na wagonjwa wote wakawa wanamsonga ili wapate kumgusa. Na watu waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu walipomwona, walijitupa chini mbele yake na kupaza sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawaamuru kwa ukali wasimjulishe kwa watu. Yesu alipanda kilimani, akawaita wale aliowataka. Basi, wakamwendea, naye akawateua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, wakae naye, awatume kuhubiri na wawe na uwezo wa kuwafukuza pepo. Basi, hao kumi na wawili walioteuliwa ndio hawa: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina, Petro), Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo (Yesu aliwapa hawa ndugu wawili jina Boanerge, maana yake “Wanangurumo”), Andrea na Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Thoma, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkanaani na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu. Kisha Yesu alikwenda nyumbani. Umati wa watu ukakusanyika tena, hata Yesu na wafuasi wake wasiweze kupata nafasi ya kula chakula. Basi, watu wa jamaa yake walipopata habari hiyo wakatoka kwenda kumchukua maana walikuwa wanasema kwamba ana wazimu. Nao waalimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu, wakasema, “Ana Beelzebuli! Tena, anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo.” Hapo Yesu akawaita, akawaambia kwa mifano, “Shetani anawezaje kumfukuza Shetani? Ikiwa utawala mmoja umegawanyika makundimakundi yanayopingana, utawala huo hauwezi kudumu. Tena, ikiwa jamaa moja imegawanyika makundimakundi yanayopingana, jamaa hiyo itaangamia. Ikiwa basi, utawala wa Shetani umegawanyika vikundivikundi hauwezi kudumu, bali utaangamia kabisa. “Hakuna mtu awezaye kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyanganya mali yake, isipokuwa kwanza amemfunga huyo mtu mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kumnyanganya mali yake. “Kweli nawaambieni, watu watasamehewa dhambi zao zote na kufuru zao zote; lakini anayesema mabaya dhidi ya Roho Mtakatifu, hatasamehewa kamwe; ana hatia ya dhambi ya milele.” ( Yesu alisema hivyo kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”) Mama yake Yesu na ndugu zake walifika hapo, wakasimama nje, wakampelekea ujumbe kumwita. Umati wa watu ulikuwa umekaa hapo kumzunguka. Basi, watu wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kukuona.” Yesu akawaambia, “Mama yangu na ndugu zangu ni kina nani?” Hapo akawatazama watu waliokuwa wamemzunguka, akasema, “Tazameni! Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu. Mtu yeyote anayefanya anayotaka Mungu, huyo ndiye kaka yangu, dada yangu na mama yangu.” Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wote wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa. Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia, “Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi, zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. Jua lilipochomoza, zikateketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka. Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikamea, zikakua na kuzaa: Moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia.” Kisha akawaambia, “Mwenye masikio na asikie!” Yesu alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliomsikia walimwendea pamoja na wale kumi na wawili, wakamwuliza juu ya hiyo mifano. Naye akawaambia, “Nyinyi mmejaliwa kujua siri ya ufalme wa Mungu, lakini wale walio nje wataambiwa kila kitu kwa mifano, ili, ‘Watazame kweli, lakini wasione. Wasikie kweli, lakini wasielewe. La sivyo, wangemgeukia Mungu, naye angewasamehe.’” Basi, Yesu akawauliza, “Je, nyinyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote? Mpanzi hupanda neno la Mungu. Watu wengine ni kama walio njiani ambapo neno lilipandwa. Lakini mara tu baada ya kulisikia, Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu walisikiapo hilo neno hulipokea kwa furaha. Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno, mara wanakata tamaa. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaosikia hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda. Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: Wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia.” Yesu akaendelea kuwaambia, “Je, watu huwasha taa wakaileta ndani na kuifunika kwa debe au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya kinara. Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila kilichofunikwa kitafunuliwa. Mwenye masikio na asikie!” Akawaambia pia, “Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa. Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.” Yesu akaendelea kusema, “Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani. Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika. Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: Kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke. Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika.” Tena, Yesu akasema, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani? Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote. Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake.” Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia. Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu. Jioni, siku hiyohiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvuke ziwa, twende ngambo.” Basi, wakauacha ule umati wa watu, wakamchukua Yesu katika mashua alimokuwa. Vilevile mashua nyingine zilimfuata. Basi, dhoruba kali ikaanza kuvuma, mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikaanza kujaa maji. Yesu alikuwa sehemu ya nyuma ya mashua, amelala juu ya mto. Basi, wanafunzi wakamwamsha na kumwambia, “Mwalimu, je, hujali kwamba sisi tunaangamia?” Basi, akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, “Kimya! Tulia!” Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa. Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mbona mnaogopa? Je, bado hamna imani?” Nao wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, “Huyu ni nani basi, hata upepo na mawimbi vinamtii?” Basi, wakafika katika nchi ya Wagerase, ngambo ya ziwa. Mara tu Yesu aliposhuka mashuani, mtu mmoja aliyepagawa na pepo mchafu alitoka makaburini, akakutana naye. Mtu huyo alikuwa akiishi makaburini wala hakuna mtu aliyeweza tena kumfunga kwa minyororo. Mara nyingi walimfunga kwa pingu na minyororo lakini kila mara aliweza kuikata hiyo minyororo na kuzivunja hizo pingu, wala hakuna mtu aliyeweza kumzuia. Mchana na usiku alikaa makaburini na milimani akipaza sauti na kujikatakata kwa mawe. Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akamwinamia akisema kwa sauti kubwa, “Una nini nami, wewe Yesu Mwana wa Mungu aliye juu? Kwa jina la Mungu, nakusihi usinitese!” ( Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, “Pepo mchafu, mtoke mtu huyu.”) Basi, Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?” Naye akajibu, “Jina langu ni ‘Jeshi,’ maana sisi tu wengi.” Kisha akamsihi Yesu asiwafukuze hao pepo katika nchi ile. Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe malishoni kwenye mteremko wa mlima. Basi, hao pepo wakamsihi, “Utupeleke kwa hao nguruwe, tuwaingie.” Naye akawaruhusu. Basi, hao pepo wachafu wakatoka, wakawaingia wale nguruwe. Kundi lote la nguruwe wapatao 2,000 likaporomoka kwenye ule mteremko mkali mpaka ziwani, likatumbukia majini. Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakatangaza jambo hilo mjini na mashambani. Watu wakafika kuona yaliyotukia. Wakamwendea Yesu, wakamwona na mtu yuleyule aliyekuwa amepagawa na jeshi la pepo ameketi chini, amevaa nguo na ana akili yake sawa, wakaogopa. Watu walioshuhudia tukio hilo wakawaeleza wengine mambo yaliyompata huyo mtu aliyekuwa amepagawa na pepo na juu ya wale nguruwe. Basi, wakaanza kumwomba aondoke katika nchi yao. Yesu alipokuwa anapanda mashuani, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamwomba amruhusu kwenda naye. Lakini Yesu akamkatalia. Badala yake akamwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako, ukawaambie mambo yote Bwana aliyokutendea na jinsi alivyokuonea huruma.” Basi, huyo mtu akaenda, akaanza kutangaza huko Dekapoli mambo yote Yesu aliyomtendea; watu wote wakashangaa. Yesu alivukia tena upande wa pili wa ziwa kwa mashua. Umati mkubwa wa watu ukakusanyika mbele yake, naye akawa amesimama kando ya ziwa. Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi aitwaye Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake, akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa karibu na kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na kuishi.” Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande. Mmojawapo alikuwa mwanamke mwenye ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Mwanamke huyo alikuwa amekwisha sumbuka sana kuwaendea waganga wengi. Na ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote, hakupata nafuu bali hali yake ilizidi kuwa mbaya. Alikuwa amesikia habari za Yesu, na hivyo akaupenya msongamano wa watu kutoka nyuma, akagusa vazi lake. Alifanya hivyo, maana alijisemea, “Nikigusa tu vazi lake, nitapona.” Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, akajisikia mwilini mwake kwamba ameponywa ugonjwa wake. Yesu alitambua mara kwamba nguvu imemtoka. Basi akaugeukia ule umati wa watu, akauliza, “Nani aliyegusa mavazi yangu?” Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi watu wanavyokusonga; mbona unauliza nani aliyekugusa?” Lakini Yesu akaendelea kutazama amwone huyo aliyefanya hivyo. Hapo huyo mwanamke, akifahamu yaliyompata, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusema ukweli wote. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.” Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?” Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, “Usiogope, amini tu.” Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi. Akaingia ndani, akawaambia, “Mbona mnapiga kelele na kulia? Msichana hakufa, amelala tu.” Lakini wao wakamcheka. Basi, akawatoa wote nje, akawachukua baba yake na mama yake huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana. Kisha akamshika mkono, akamwambia, “Talitha, kumi,” maana yake, “Msichana, nakuambia, amka!” Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi. Yesu akawakataza sana wasimjulishe mtu jambo hilo. Kisha akawaambia wampe huyo msichana chakula. Yesu aliondoka hapo akaenda katika kijiji chake, akifuatwa na wanafunzi wake. Siku ya Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sunagogi. Wengi waliomsikia walishangaa, wakasema, “Je, ameyapata wapi mambo haya? Ni hekima gani hii aliyopewa? Tena, anatendaje maajabu haya anayoyafanya? Je, huyu si yule seremala, mwana wa Maria, na ndugu yao kina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni? Je, dada zake si wanaishi papa hapa kwetu?” Basi, wakawa na mashaka naye. Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika nchi yake, kwa jamaa zake na nyumbani mwake.” Hakuweza kutenda miujiza hapo, ila aliwawekea mikono wagonjwa wachache, akawaponya. Alishangaa sana kwa sababu ya kutoamini kwao. Kisha Yesu alivitembelea vijiji vya pale karibu akiwafundisha watu. Aliwaita wale wanafunzi kumi na wawili, akaanza kuwatuma wawiliwawili. Aliwapa uwezo wa kuwafukuza pepo wachafu; akawaamuru: “Msichukue chochote mnapokwenda isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kibindoni. Vaeni viatu lakini msichukue koti la ziada.” Tena aliwaambia, “Popote mtakapokaribishwa nyumbani, kaeni humo mpaka mtakapoondoka mahali hapo. Mahali popote ambapo watu watakataa kuwakaribisheni au kuwasikiliza, ondokeni hapo na kuyakunguta mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.” Basi, wakaondoka, wakahubiri watu watubu. Waliwafukuza pepo wengi wabaya; wakawapaka mafuta wagonjwa wengi, wakawaponya. Basi, mfalme Herode alisikia juu ya hayo yote, maana sifa za Yesu zilienea kila mahali. Baadhi ya watu walikuwa wakisema, “Yohane Mbatizaji amefufuka kutoka kwa wafu, ndiyo maana nguvu hizi zinafanya kazi ndani yake.” Wengine walisema, “Mtu huyu ni Elia.” Wengine walisema, “Huyu ni nabii kama mmojawapo wa manabii wa kale.” Lakini Herode alipopata habari hizi alisema, “Huyu ni Yohane! Nilimkata kichwa, lakini amefufuka.” Hapo awali Herode mwenyewe alikuwa ameamuru Yohane atiwe nguvuni, akamfunga gerezani. Herode alifanya hivyo kwa sababu ya Herodia ambaye Herode alimwoa ingawaje alikuwa mke wa Filipo, ndugu yake. Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kumchukua mke wa ndugu yako.” Basi, Herodia alimchukia sana Yohane, akataka kumuua, asiweze. Herode alimwogopa Yohane kwa maana alijua kwamba yeye ni mtu mwema na mtakatifu, na hivyo akamlinda. Herode alipenda kumsikiliza Yohane, ingawaje baada ya kumsikiliza, alifadhaika sana. Ndipo ikapatikana nafasi, wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode. Herode aliwafanyia karamu wazee wa baraza lake, majemadari na viongozi wa Galilaya. Basi, binti yake Herodia aliingia, akacheza, akawafurahisha sana Herode na wageni wake. Mfalme akamwambia huyo msichana, “Niombe chochote utakacho, nami nitakupa.” Tena akamwapia, “Chochote utakachoniomba, nitakupa; hata ikiwa ni nusu ya ufalme wangu.” Hapo huyo msichana akatoka, akamwuliza mama yake, “Niombe nini?” Naye akamjibu, “Kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Msichana akamrudia mfalme mbio akamwomba, “Nataka unipe sasa hivi katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Mfalme akahuzunika sana, lakini kwa sababu ya kiapo chake, na kwa ajili ya wale wageni wake karamuni, hakutaka kumkatalia. Basi, mfalme akamwamuru askari kukileta kichwa cha Yohane. Askari akaenda, akamkata kichwa Yohane mle gerezani, akakileta katika sinia, akampa msichana naye msichana akampa mama yake. Wanafunzi wa Yohane walipopata habari, walikwenda wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini. Wale mitume walirudi, wakakusanyika mbele ya Yesu, wakamwarifu yote waliyotenda na kufundisha. Yesu akawaambia, “Twendeni peke yetu mpaka mahali pa faragha mkapumzike kidogo.” Alisema hivyo kwa kuwa kulikuwa na watu wengi mno waliokuwa wanafika hapo na kuondoka hata Yesu na wanafunzi wake hawakuweza kupata nafasi ya kula chakula. Basi, wakaondoka peke yao kwa mashua, wakaenda mahali pa faragha. Lakini watu wengi waliwaona wakienda, wakawatambua. Hivyo wengi wakatoka katika kila mji, wakakimbilia huko Yesu na wanafunzi wake walikokuwa wanakwenda, wakawatangulia kufika. Aliposhuka pwani, Yesu aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Akaanza kuwafundisha mambo mengi. Saa za mchana zilikwisha pita. Basi, wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na sasa kunakuchwa. Afadhali uwaage watu waende mashambani na katika vijiji vya jirani, wanunue chakula.” Lakini Yesu akawaambia, “Wapeni nyinyi chakula.” Nao wakamwuliza, “Je, twende kununua mikate kwa fedha dinari 200, na kuwapa chakula?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi? Nendeni kutazama.” Walipokwisha tazama, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.” Basi, Yesu akawaamuru wanafunzi wawaketishe watu wote makundimakundi penye nyasi. Nao wakaketi makundimakundi ya watu 100 na ya watu hamsini. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki, akaimega mikate, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. Na wale samaki wawili pia akawagawia wote. Watu wote wakala, wakashiba. Wakaokota mabaki ya mikate na samaki pia, wakajaza vikapu kumi na viwili. Nao waliokula hiyo mikate walikuwa wanaume 5,000. Mara Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie kwenda Bethsaida, ngambo ya ziwa, wakati yeye anauaga umati wa watu. Baada ya kuwaaga watu alikwenda mlimani kusali. Ilipokuwa jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, naye alikuwa peke yake katika nchi kavu. Basi, akawaona wanafunzi wake wakitaabika kwa kupiga makasia, maana upepo ulikuwa unawapinga. Karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji, akataka kuwapita. Lakini walipomwona akitembea juu ya maji, walidhani ni mzimu, wakapiga yowe. Maana wote walipomwona waliogopa sana. Mara Yesu akasema nao, “Tulieni, ni mimi. Msiogope!” Kisha akapanda mashuani walimokuwa, na upepo ukatulia. Nao wakashangaa sana, kwa sababu hawakuwa bado wameelewa maana ya ile mikate. Akili zao zilikuwa bado zimepumbazika. Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. Walipotoka mashuani watu walimtambua Yesu mara. Basi, kwa haraka wakazunguka katika nchi ile yote, wakaanza kuwachukua wagonjwa wamelala juu ya mikeka yao, wakawapeleka kila mahali waliposikia Yesu yupo. Kila mahali Yesu alipokwenda, vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa uwanjani, wakamsihi waguse walau pindo la vazi lake. Nao wote waliomgusa walipona. Baadhi ya Mafarisayo na waalimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu. Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa. Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: Hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo. Tena, hawali kitu chochote kutoka sokoni, mpaka wamekiosha kwanza. Kuna pia desturi nyingine walizozipokea toka zamani kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba. Basi, Mafarisayo na waalimu wa sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati mapokeo tuliyoyapokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?” Yesu akawajibu, “Wanafiki nyinyi! Nabii Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu alipoandika: ‘Mungu asema: Watu hawa, huniheshimu kwa maneno tu, lakini mioyoni mwao, wako mbali nami. Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’ Nyinyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu.” Yesu akaendelea kusema, “Nyinyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu! Maana Mose aliamuru: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima afe’. Lakini nyinyi mwafundisha, ‘Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani zawadi kwa Mungu), basi, halazimiki tena kumsaidia baba yake au mama yake’. Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo.” Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, mkaelewe. Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu kutoka nje kinachoweza kumtia mtu unajisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu unajisi.” Mwenye masikio na asikie! Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano. Naye akawaambia, “Je, hata nyinyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu kutoka nje, hakiwezi kumtia unajisi, kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?” (Kwa kusema hivyo, Yesu alihalalisha vyakula vyote.) Akaendelea kusema, “Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia unajisi. Maana kutoka ndani, moyoni mwa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu. Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu unajisi.” Yesu aliondoka hapo, akaenda wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha. Hapo mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake. Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu. Yesu akamwambia, “Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Lakini huyo mama akasema, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.” Yesu akamwambia, “Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!” Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka. Kisha Yesu aliondoka wilaya ya Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli. Basi, wakamletea bubu kiziwi, wakamwomba amwekee mikono. Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi. Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, “Efatha,” maana yake “Funguka.” Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa. Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo. Watu walishangaa sana, wakasema, “Amefanya yote vyema: Amewajalia viziwi kusikia, na mabubu kusema!” Wakati huo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena, na hawakuwa na chakula. Basi, Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa watazimia njiani, maana baadhi yao wametoka mbali.” Wanafunzi wake wakamwuliza, “Hapa nyikani itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba.” Basi, akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia. Walikuwa pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki, akaamuru vigawiwe watu vilevile. Watu wakala, wakashiba. Wakakusanya makombo wakajaza vikapu saba. Nao waliokula walikuwa watu wapatao 4,000. Yesu akawaaga, na mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha. Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka afanye ishara kutoka mbinguni. Yesu akahuzunika rohoni, akasema, “Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote.” Basi, akawaacha, akapanda tena mashua, akaanza safari kwenda ngambo ya pili ya ziwa. Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika mashua. Yesu akawaonya, “Angalieni sana! Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.” Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao, “Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate.” Yesu alitambua hayo, akawaambia, “Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu ni mizito? Je, mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu 5,000? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki.” Wakamjibu, “Kumi na viwili.” “Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki?” Wakamjibu, “Saba.” Basi, akawaambia, “Na bado hamjaelewa?” Yesu alifika Bethsaida pamoja na wanafunzi wake. Huko watu wakamletea kipofu, wakamwomba amguse. Yesu akamshika huyo kipofu mkono, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni, akamwekea mikono, akamwuliza, “Je, unaweza kuona kitu?” Huyo kipofu akatazama, akasema, “Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea.” Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa. Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, “Usirudi kijijini!” Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?” Wakamjibu, “Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia na wengine mmojawapo wa manabii.” Naye akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo.” Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake. Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake kwamba ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Kwamba atauawa, na baada ya siku tatu atafufuka. Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Hapo, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea. Lakini Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, “Ondoka mbele yangu Shetani! Mawazo yako si ya kimungu ila ni ya kibinadamu.” Kisha akauita umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. Maana mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu anayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, atayaokoa. Je, kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake? Ama mtu atatoa kitu gani badala ya maisha yake? Mtu yeyote katika kizazi hiki kiovu na kisicho na uaminifu kwa Mungu, anayenionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo, wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.” Yesu akaendelea kuwaambia, “Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa enzi.” Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao, mavazi yake yakangaa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe. Elia na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu. Petro akamwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri sisi kuwapo hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema. Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni.” Mara wanafunzi hao wakatazama tena, lakini hawakumwona mtu mwingine, ila Yesu peke yake pamoja nao. Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu aliwakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu. Basi, wakashika agizo hilo, lakini wakawa wanajadiliana wao kwa wao maana ya kufufuka kutoka kwa wafu. Wakamwuliza Yesu, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ni lazima kwanza Elia aje?” Naye akawajibu, “Naam, Elia anakuja kwanza kutayarisha yote. Hata hivyo, kwa nini basi imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Mwana wa Mtu atapatwa na mateso mengi na kudharauliwa? Lakini nawaambieni, Elia amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyotaka kama ilivyoandikwa juu yake.” Walipowafikia wale wanafunzi wengine, waliona umati mkubwa wa watu hapo. Na baadhi ya waalimu wa sheria walikuwa wanajadiliana nao. Mara tu ule umati wa watu ulipomwona, wote walishangaa sana, wakamkimbilia wamsalimu. Yesu akawauliza, “Mnajadiliana nini nao?” Hapo mtu mmoja katika ule umati wa watu akamjibu, “Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo aliyemfanya kuwa bubu. Kila mara anapomvamia, humwangusha chini na kumfanya atokwe na povu kinywani, akisaga meno na kuwa mkavu mwili wote. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo lakini hawakuweza.” Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kwangu.” Wakampeleka. Mara tu huyo pepo alipomwona Yesu, alimtia mtoto kifafa, naye mtoto akaanguka chini, akagaagaa na kutoka povu kinywani. Yesu akamwuliza baba yake huyo mtoto, “Amepatwa na mambo hayo tangu lini?” Naye akamjibu, “Tangu utoto wake. Na mara nyingi pepo huyo amemwangusha motoni na majini, ili amwangamize kabisa. Basi, ikiwa waweza, utuhurumie na kutusaidia!” Yesu akamwambia, “Ati ikiwa waweza! Mambo yote yanawezekana kwa mtu aliye na imani.” Hapo, huyo baba akalia kwa sauti, “Naamini! Lakini imani yangu haitoshi, nisaidie.” Yesu alipouona umati wa watu unaongezeka upesi mbele yake, alimkemea yule pepo mchafu “Pepo unayemfanya huyu mtoto kuwa bubu na kiziwi, nakuamuru, mtoke mtoto huyu wala usimwingie tena!” Hapo huyo pepo alipaza sauti, akamwangusha huyo mtoto chini, kisha akamtoka. Mtoto alionekana kama maiti, hata wengine walisema, “Amekufa!” Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama. Basi, Yesu alipoingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza kwa faragha, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?” Naye akawaambia, “Pepo wa aina hii hawezi kutoka isipokuwa kwa sala.” Yesu na wanafunzi wake waliondoka hapo, wakaendelea na safari kupitia wilaya ya Galilaya. Yesu hakupenda watu wajue alipokuwa, kwa sababu alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Aliwaambia, “Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu ambao watamuua; lakini siku ya tatu baada ya kuuawa atafufuka.” Wanafunzi hawakufahamu jambo hilo. Wakaogopa kumwuliza. Basi, walifika Kafarnaumu. Na alipokuwa nyumbani, aliwauliza, “Mlikuwa mnajadiliana nini njiani?” Lakini wao wakanyamaza, maana njiani walikuwa wamebishana ni nani aliyekuwa mkubwa kati yao. Yesu akaketi chini, akawaita wale kumi na wawili, akawaambia, “Mtu akitaka kuwa wa kwanza lazima awe wa mwisho na mtumishi wa wote.” Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kati yao, akamkumbatia, halafu akawaambia, “Anayempokea mtoto kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, hanipokei mimi tu, bali anampokea yule aliyenituma.” Yohane akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako, nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu.” Lakini Yesu akasema, “Msimkataze, maana hakuna mtu anayefanya mwujiza kwa jina langu, na papo hapo akaweza kusema mabaya juu yangu. Maana, asiyepingana nasi, yuko upande wetu. Mtu yeyote atakayewapeni kikombe cha maji ya kunywa, kwa sababu nyinyi ni watu wake Kristo, hakika hatakosa kupata tuzo lake. “Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali kwa mtu huyo kufungiwa shingoni mwake jiwe kubwa la kusagia na kutupwa baharini. Mkono wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uhai bila mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili na kwenda katika moto wa Jehanamu. [ Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki.] Na mguu wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uhai bila mguu mmoja, kuliko kuwa na miguu yote miwili na kutupwa katika moto wa Jehanamu. [ Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki.] Na jicho lako likikukosesha, lingoe! Afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja tu, kuliko kuwa na macho yako yote mawili na kutupwa katika moto wa Jehanamu. Humo wadudu wake hawafi, na huo moto hauzimiki. “Maana kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto. Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini? Muwe na chumvi ndani yenu na kudumisha amani kati yenu.” Yesu alitoka hapo akaenda mkoani Yudea, hata ngambo ya mto Yordani. Umati wa watu ukamwendea tena, naye akawafundisha tena kama ilivyokuwa desturi yake. Basi, Mafarisayo wakamwendea, na kwa kumjaribu wakamwuliza, “Je, ni halali mume kumpa mkewe talaka?” Yesu akawajibu, “Mose aliwapa maagizo gani?” Nao wakasema, “Mose aliagiza mume kumpatia mkewe hati ya talaka na kumwacha.” Yesu akawaambia, “Mose aliwaandikia amri hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu aliumba mwanamume na mwanamke. Hivyo mwanamume atawaacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja. Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja. Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe.” Walipoingia tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake walimwuliza juu ya jambo hilo. Naye akawaambia, “Anayemwacha mkewe na kuoa mwingine, anazini dhidi ya mkewe. Na mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini.” Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea. Yesu alipoona hivyo, alikasirika akawaambia, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa. Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia humo.” Kisha akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki. Yesu alipoanza tena safari yake, mtu mmoja alimjia mbio, akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanyeje niupate uhai wa milele?” Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake. Unazijua amri: ‘Usizini, Usiue, Usiibe, Usitoe ushahidi wa uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.’” Naye akamjibu, “Mwalimu, hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu.” Yesu akamtazama, akampenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja: Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha uje unifuate.” Aliposikia hayo, alisikitika, akaenda zake akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Jinsi gani itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu!” Wanafunzi walishangazwa na maneno yake. Yesu akawaambia tena, “Watoto wangu, ni vigumu sana kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni rahisi zaidi ngamia kupenya katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Wanafunzi wake wakashangaa sana wakaulizana, “Ni nani basi, atakayeweza kuokoka?” Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa binadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si hivyo, maana kwa Mungu mambo yote huwezekana.” Petro akamwambia, “Na sisi je? Tumeacha yote, tukakufuata!” Yesu akasema, “Kweli nawaambieni, kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au mama, au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, atapokea mara mia zaidi wakati huu wa sasa: Nyumba, ndugu, dada, mama, watoto na mashamba pamoja na mateso; na katika wakati ujao atapokea uhai wa milele. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.” Basi, walikuwa njiani kwenda juu Yerusalemu, na Yesu alikuwa anawatangulia. Wanafunzi wake walijawa na hofu, na watu waliofuata waliogopa. Yesu akawachukua tena kando wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia yale yatakayompata: “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waalimu wa sheria, nao watamhukumu auawe na kumkabidhi kwa watu wa mataifa. Nao watamdhihaki; watamtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua. Lakini baada ya siku tatu atafufuka.” Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.” Yesu akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakamjibu, “Uturuhusu kuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.” Yesu akawaambia, “Hamjui mnaomba nini! Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa, au kubatizwa kama nitakavyobatizwa?” Wakamjibu, “Tunaweza.” Yesu akawaambia, “Kikombe nitakachokunywa mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa. Lakini ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga bali nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa.” Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na Yohane. Hivyo, Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao. Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkubwa kati yenu, sharti awe mtumishi wenu. Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote. Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.” Basi, wakafika Yeriko, naye Yesu alipokuwa anatoka katika mji huo akiwa na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu, mwana wa Timayo aitwaye Bartimayo, alikuwa ameketi kando ya barabara, anaomba maskini. Aliposikia kwamba ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita mahali hapo, alianza kupaza sauti, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!” Watu wengi walimkemea ili anyamaze, lakini yeye akazidi kupaza sauti, “Mwana wa Daudi, nihurumie!” Yesu alisimama, akasema, “Mwiteni.” Basi, wakamwita huyo kipofu, wakamwambia, “Jipe moyo! Simama, anakuita.” Naye akatupilia mbali vazi lake, akaruka juu, akamwendea Yesu. Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Huyo kipofu akamwambia, “Mwalimu, naomba nipate kuona.” Yesu akamwambia, “Nenda, imani yako imekuponya.” Mara huyo kipofu akaweza kuona, akamfuata Yesu njiani. Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwanapunda amefungwa, ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete. Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnafanya hivyo?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara.’” Basi, wakaenda, wakamkuta mwanapunda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua, baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua huyo mwanapunda?” Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao. Wakampelekea Yesu huyo mwanapunda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwanapunda na Yesu akaketi juu yake. Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani. Watu wote waliotangulia na wale waliofuata, wakapaza sauti zao wakisema, “Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Ubarikiwe ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Sifa kwa Mungu juu mbinguni!” Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili. Kesho yake, walipokuwa wanatoka Bethania, Yesu aliona njaa. Basi, akaona kwa mbali mtini wenye majani mengi. Akauendea ili aone kama ulikuwa na tunda lolote. Alipoufikia, aliukuta bila tunda lolote ila tu majani matupu, kwa vile hayakuwa majira yake ya matunda. Hapo akauambia mtini, “Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako.” Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo. Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia hekaluni akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha, na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Hakumruhusu mtu yeyote kupitia hekaluni akichukua kitu. Kisha akawafundisha, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote!’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi!” Makuhani wakuu na waalimu wa sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake. Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini. Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi. Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!” Yesu akawaambia, “Mwaminini Mungu. Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo. Kwa hiyo nawaambieni, mnaposali na kuomba kitu, aminini kwamba mmekipokea, nanyi mtapewa. Mnaposimama kusali, msameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe nyinyi makosa yenu.” [ Lakini msipowasamehe wengine, hata Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe nyinyi makosa yenu.] Basi, wakafika tena Yerusalemu. Yesu alipokuwa akitembea hekaluni, makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee walimwendea, wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani aliyekupa mamlaka ya kufanya mambo haya?” Lakini Yesu akawaambia, “Nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, nami pia nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka mbinguni ama kwa watu? Nijibuni.” Wakaanza kujadiliana, “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni’, atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’ Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu (Waliogopa umati wa watu maana wote waliamini kwamba Yohane alikuwa kweli nabii.) Basi, wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.” Yesu alianza kusema nao kwa mifano: “Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu. Akalizungushia ukuta, na katikati yake akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga mnara pia. Akalikodisha shamba hilo kwa wakulima, akasafiri hadi nchi ya mbali. Wakati wa mavuno, alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima, akamletee sehemu ya mazao ya shamba lake. Wale wakulima wakamkamata, wakampiga, wakamrudisha mikono mitupu. Akamtuma tena mtumishi mwingine; huyu pia wakamwumiza kichwa na kumtendea vibaya. Yule mwenye shamba akatuma mtumishi mwingine tena ambaye hao wakulima walimuua. Wengine wengi waliotumwa, baadhi yao walipigwa, na wengi wakauawa. Alibakiwa bado na mtu mmoja, yaani mwanawe mpenzi. Mwishowe akamtuma huyo akisema, ‘Watamjali mwanangu.’ Lakini hao wakulima wakaambiana, ‘Huyu ndiye mrithi, basi, tumuue ili urithi wake uwe wetu!’ Kwa hiyo wakamkamata, wakamuua na kumtupa nje ya lile shamba la mizabibu. “Basi, mwenye shamba atafanya nini? Atakuja kuwaangamiza hao wakulima na kulikodisha hilo shamba la mizabibu kwa watu wengine. Je, hamjasoma Maandiko haya? ‘Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi. Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu.’” Makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee walifahamu ya kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu. Kwa hiyo walijaribu kumtia nguvuni, lakini waliogopa umati wa watu. Basi, wakamwacha, wakaenda zao. Basi, baadhi ya Mafarisayo na wafuasi wa kikundi cha Herode walitumwa ili wamtege Yesu kwa maneno yake. Wakamwendea, wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu unayesema ukweli mtupu, wala humjali mtu yeyote. Wala cheo cha mtu si kitu kwako, lakini wafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la? Tulipe au tusilipe?” Lakini Yesu alijua unafiki wao, akawaambia, “Mbona mnanijaribu? Nionesheni hiyo sarafu.” Wakamwonesha. Naye akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Basi, Yesu akawaambia, “Ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” Wakashangazwa sana naye. Masadukayo ambao husema kwamba hakuna ufufuo walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Mwalimu, Mose alituagiza hivi: ‘Mtu akifa na kuacha mke bila mtoto, ndugu yake lazima amchukue huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto.’ Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa, akafa bila kuacha mtoto. Ndugu wa pili akamwoa huyo mjane, naye pia akafa bila kuacha mtoto; na ndugu watatu hali kadhalika. Wote saba walikufa bila kuacha mtoto. Mwishowe yule mama mjane naye akafa. Basi, siku watu watakapofufuka, mama huyo atakuwa mke wa nani? Wote saba walikuwa wamemwoa.” Yesu akawaambia, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika wa mbinguni. Lakini kuhusu kufufuliwa kwa wafu, je, hamjasoma kitabu cha Mose katika sehemu inayohusu kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto? Mungu alimwambia Mose, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo.’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Nyinyi mmekosea sana.” Mmojawapo wa waalimu wa sheria alifika, akasikia mabishano yao. Alipoona kwamba Yesu aliwajibu vyema, akajitokeza, akamwuliza, “Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?” Yesu akamjibu, “Ya kwanza ndiyo hii: ‘Sikiliza Israeli! Bwana Mungu wetu, ndiye peke yake Bwana. Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote.’ Na ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ Hakuna amri nyingine iliyo kubwa zaidi kuliko hizi.” Basi, yule mwalimu wa sheria akamwambia, “Vyema Mwalimu! Umesema ukweli kwamba Mungu ni mmoja tu wala hakuna mwingine ila yeye. Na ni lazima mtu kumpenda Mungu kwa moyo wote, kwa akili yote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani yake kama anavyojipenda mwenyewe. Jambo hili ni muhimu zaidi kuliko tambiko na sadaka zote za kuteketezwa.” Yesu alipoona kwamba huyu mtu alimjibu kwa ujasiri, akamwambia, “Wewe huko mbali na ufalme wa Mungu.” Baada ya hayo, hakuna mtu aliyethubutu tena kumwuliza kitu. Wakati Yesu alipokuwa akifundisha hekaluni, aliuliza, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ya kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? Daudi mwenyewe akiongozwa na Roho Mtakatifu alisema: ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke maadui zako chini ya miguu yako.’ “Daudi mwenyewe anamwita Kristo Bwana. Basi, Kristo atakuwaje mwanawe?” Umati wa watu ulikuwa ukimsikiliza kwa furaha. Katika mafundisho yake, Yesu alisema, “Jihadharini na waalimu wa sheria ambao hupenda kupitapita wamejivalia kanzu ndefu na kusalimiwa na watu kwa heshima sokoni; hupenda kuketi mahali pa heshima katika masunagogi, na kuchukua nafasi za heshima katika karamu. Huwadhulumu wajane huku wakijisingizia kusali sala ndefu! Siku ya hukumu watapata adhabu kali.” Yesu alikuwa ameketi karibu na sanduku la hazina. Akawa anatazama jinsi watu wengi walivyokuwa wakitoa fedha na kuzitia katika hazina ya hekalu. Matajiri wengi walitoa fedha nyingi. Hapo akaja mama mmoja mjane maskini, akatoa sarafu mbili ndogo za fedha. Hapo Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Kweli nawaambieni, mama huyu mjane maskini ametia katika sanduku la hazina kiasi kikubwa kuliko walichotia wengine wote. Maana wengine wote walitoa kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa yote aliyokuwa nayo, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi.” Yesu alipokuwa anatoka hekaluni mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, “Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!” Yesu akamwambia, “Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa.” Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha, “Tuambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?” Yesu akaanza kuwaambia, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, kila mmoja akisema kuwa yeye ni mimi! Nao watawapotosha watu wengi. Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado. Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto. “Lakini nyinyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, ili mpate kunishuhudia kwao. Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote. Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si nyinyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu. Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanawe; watoto nao watawashambulia wazazi wao na kuwaua. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa. “Mtakapoona ‘Chukizo Haribifu limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake), hapo, walioko Yudea wakimbilie milimani. Aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu. Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi. Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena. Kama Bwana asingepunguza siku hizo hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo. “Basi mtu akiwaambieni, ‘Tazama, Kristo yupo hapa,’ au ‘Yupo pale,’ msimsadiki. Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, kwa ajili ya kuwapotosha wateule wa Mungu kama ikiwezekana. Lakini nyinyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea. “Basi, siku hizo, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza. Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu. Kisha atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu. “Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa mavuno umekaribia. Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana. Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. “Lakini, juu ya siku au saa hiyo hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini. Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia na mlinzi wa mlango awe macho. Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi. Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala. Ninayowaambieni nyinyi, nawaambia wote: Kesheni!” Ilikuwa siku mbili tu kabla ya sikukuu ya Pasaka na ya mikate isiyotiwa chachu. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila, wamuue. Lakini walisema, “Tusimtie nguvuni wakati wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia.” Yesu alikuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni Mkoma. Alipokuwa mezani kula chakula, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya nardo safi ya thamani kubwa alikuja, akaivunja hiyo chupa, akammiminia Yesu marashi hayo kichwani. Baadhi ya watu waliokuwa hapo walikasirika, wakajisemea, “Kwa nini kupoteza ovyo marashi haya? Yangaliweza kuuzwa kwa fedha kiasi cha dinari 300, wakapewa maskini!” Wakamkemea huyo mama. Lakini Yesu akawaambia, “Mwacheni; kwa nini mnamsumbua? Amenitendea jambo jema. Maskini mnao daima pamoja nanyi; mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima. Yeye amefanya alivyoweza; ameupaka mwili wangu marashi kuutayarisha kwa mazishi. Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni Habari Njema itakapohubiriwa, kitendo hiki alichofanya kitatajwa kwa kumkumbuka yeye.” Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, alikwenda kwa makuhani wakuu ili kumsaliti Yesu. Makuhani wakuu waliposikia habari hizo, walifurahi, wakamwahidi kumpa fedha. Basi, Yuda akaanza kutafuta nafasi ya kumsaliti. Siku ya kwanza ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wakati ambapo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wake walimwuliza, “Wataka tukuandalie wapi karamu ya Pasaka?” Basi Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake akiwaambia, “Nendeni mjini, na humo mtakutana na mwanamume mmoja anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka katika nyumba atakayoingia, mkamwambie mwenye nyumba, ‘Mwalimu anasema: Wapi chumba changu ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani kilichotayarishwa na kupambwa. Tuandalieni humo.” Wanafunzi wakaondoka, wakaenda mjini, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia. Wakaandaa karamu ya Pasaka. Ilipokuwa jioni, Yesu alifika pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Walipokuwa mezani wakila, Yesu alisema, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu anayekula pamoja nami, atanisaliti.” Hapo wanafunzi wake wakaanza kuhuzunika, wakamwuliza mmojammoja, “Je, ni mimi?” Yesu akawaambia, “Ni mmoja wenu nyinyi kumi na wawili, anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli. Kweli Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yanavyosema juu yake; lakini, ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa!” Walipokuwa wanakula, Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni; huu ni mwili wangu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akamshukuru Mungu, akawapa; wote wakanywa kutoka kikombe hicho. Akawaambia, “Hii ni damu yangu inayothibitisha agano la Mungu, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi. Kweli nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika ufalme wa Mungu.” Kisha wakaimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Nyinyi nyote mtakuwa na mashaka nami; maana Maandiko Matakatifu yasema: ‘Nitampiga mchungaji, nao kondoo watatawanyika.’ Lakini nikisha fufuka, nitawatangulieni kule Galilaya.” Petro akamwambia “Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakukana kamwe!” Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakuacha kamwe.” Wanafunzi wote pia wakasema vivyo hivyo. Basi, wakafika katika bustani iliyoitwa Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati mimi nasali.” Kisha akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa na kukesha.” Akaenda mbele kidogo, akajitupa chini kifudifudi, akasali kwamba, kama ingewezekana, asiipitie saa hiyo ya mateso. Akasema, “Baba yangu, kwako mambo yote yanawezekana. Uniondolee kikombe hiki; lakini isiwe kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.” Kisha akarudi kwa wanafunzi wale watatu, akawakuta wamelala. Basi, akamwuliza Petro, “Simoni, je, umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja?” Kisha akawaambia, “Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka, lakini mwili ni dhaifu.” Akaenda kusali tena akirudia maneno yaleyale. Kisha akarudi tena, akawakuta wamelala. Macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Hawakujua la kumjibu. Alipowajia mara ya tatu aliwaambia, “Mnalala bado na kupumzika? Sasa imetosha! Saa imefika! Mwana wa Mtu anakabidhiwa kwa watu waovu. Amkeni, twende zetu. Tazameni, yule atakayenisaliti amekaribia.” Yesu alipokuwa bado anasema, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika pamoja na umati wa watu wenye mapanga na marungu. Watu hao walikuwa wametumwa na makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee. Msaliti Yuda alikuwa amewapa ishara: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi.” Yuda alipofika tu, alimwendea Yesu moja kwa moja, akamwambia, “Mwalimu!” Kisha akambusu. Basi, hao watu wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. Mmoja wa wale waliokuwa wamesimama hapo pamoja na Yesu, akachomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Yesu akawaambia, “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Kila siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini sasa lazima Maandiko Matakatifu yatimie.” Hapo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa anamfuata Yesu akiwa amevaa shuka. Nao wakajaribu kumkamata. Lakini yeye akaponyoka, akaiachilia ile shuka, akakimbia uchi. Basi, wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu ambapo makuhani wakuu wote, wazee na waalimu wa sheria walikuwa wamekutanika. Petro alimfuata Yesu kwa mbali, akaingia ndani ya ua wa kuhani mkuu, akaketi pamoja na walinzi akiota moto. Makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa kumshtaki Yesu wapate kumwua, lakini hawakuupata. Watu wengi walitoa ushahidi wa uongo juu ya Yesu, lakini ushahidi wao haukupatana. Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uongo wakisema: “Tulimsikia mtu huyu akisema, ‘Nitaliharibu hekalu hili lililojengwa kwa mikono, na kwa siku tatu nitajenga lingine lisilojengwa kwa mikono.’” Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukupatana. Basi, kuhani mkuu akasimama katikati yao, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?” Lakini yeye akakaa kimya; hakusema hata neno moja. Kuhani mkuu akamwuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Mtukufu?” Yesu akajibu, “Naam, mimi ndiye. Tena, mtamwona Mwana wa Mtu amekaa upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija katika mawingu ya mbinguni.” Hapo kuhani mkuu akararua joho lake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake! Nyinyi mwaonaje?” Wote wakaamua kwamba anastahili kuuawa. Basi, baadhi yao wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, wakampiga na kumwambia, “Bashiri ni nani amekupiga!” Hata watumishi wakamchukua, wakampiga makofi. Petro alipokuwa bado chini uani, mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu alikuja. Alipomwona Petro akiota moto, alimtazama, akamwambia, “Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.” Lakini Petro akakana, “Sijui, wala sielewi unayosema!” Kisha Petro akaondoka, akaenda nje uani. Hapo jogoo akawika. Yule mtumishi alipomwona tena Petro, akaanza tena kuwaambia watu waliokuwa wamesimama hapo, “Mtu huyu ni mmoja wao.” Petro akakana tena. Baadaye kidogo, watu waliokuwa wamesimama hapo wakamwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, maana wewe ni Mgalilaya.” Lakini Petro akaanza kulaani na kuapa akisema, “Mimi simjui mtu huyu mnayesema habari zake.” Hapo jogoo akawika mara ya pili. Basi, Petro akakumbuka jinsi Yesu alivyokuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Petro akabubujika machozi. Kulipopambazuka, makuhani wakuu walifanya shauri pamoja na wazee, waalimu wa sheria na Baraza lote, wakamfunga Yesu pingu, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato. Pilato akamwuliza Yesu, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Wewe umesema.” Makuhani wakuu wakamshtaki Yesu mambo mengi. Pilato akamwuliza tena Yesu, “Je, hujibu neno? Tazama wanavyotoa mashtaka mengi juu yako.” Lakini Yesu hakujibu neno, hata Pilato akashangaa. Kila wakati wa sikukuu ya Pasaka, Pilato alikuwa na desturi ya kuwafungulia mfungwa mmoja waliyemtaka. Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Baraba, ambaye alikuwa amefungwa pamoja na waasi wengine kwa kusababisha uasi na mauaji. Watu wengi wakamwendea Pilato wakamwomba awafanyie kama kawaida yake. Pilato akawauliza, “Je, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?” Alisema hivyo kwa sababu alijua wazi kwamba makuhani wakuu walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu ya wivu. Lakini makuhani wakuu wakawachochea watu wamwombe Pilato awafungulie Baraba. Pilato akawauliza tena, “Basi, sasa mwataka nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?” Watu wote wakapaza sauti tena: “Msulubishe!” Lakini Pilato akawauliza, “Kwa nini! Amefanya ubaya gani?” Lakini wao wakazidi kupaza sauti, “Msulubishe!” Pilato alitaka kuuridhisha huo umati wa watu; basi, akamwachilia Baraba kutoka gerezani. Akaamuru Yesu apigwe viboko, kisha akamtoa asulubiwe. Kisha askari walimpeleka Yesu ndani ukumbini, katika ikulu, wakakusanya kikosi kizima cha askari. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamwekea kichwani. Wakaanza kumsalimu, “Shikamoo Mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate; wakampigia magoti na kumsujudia. Baada ya kumdhihaki, walimvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha. Walipokuwa njiani, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni, mwenyeji wa Kurene. Yeye alikuwa baba yao Aleksanda na Rufo, na wakati huo alikuwa akitoka shambani. Basi, wakamlazimisha achukue msalaba wa Yesu. Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa. Wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini yeye alikataa kunywa. Basi, wakamsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura waamue nani angepata nini. Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha. Na shtaka dhidi yake lilikuwa limeandikwa, “Mfalme wa Wayahudi.” Pamoja naye waliwasulubisha wanyanganyi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. [ Hapo yakatimia Maandiko Matakatifu yanayosema, “Aliwekwa kundi moja na waovu.”] Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana, wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe mwenye kuvunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu! Sasa, shuka msalabani ujiokoe mwenyewe!” Nao makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Ati yeye ni Kristo, Mfalme wa Israeli! Basi, na ashuke kutoka msalabani ili tuone na kuamini.” Hata watu wale waliosulubiwa pamoja naye walimtukana. Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa giza likaikumba nchi yote. Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, akasema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, “Sikiliza! Anamwita Elia.” Mtu mmoja akakimbia, akaichovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe akisema, “Hebu tuone kama Elia atakuja kumteremsha msalabani!” Yesu akapaza sauti kubwa, akakata roho. Basi, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini. Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake alipoona kwamba Yesu alikata roho namna hiyo, akasema, “Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!” Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria Magdalene, Salome, na Maria mama wa kina Yakobo mdogo na Yose. Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia. Kulikuwa na wanawake wengine wengi waliokuja Yerusalemu pamoja naye. Wakati wa jioni ulikuwa umekwisha fika. Hiyo ilikuwa siku ya Maandalio, yaani siku inayotangulia Sabato. Hapo akaja Yosefu mwenyeji wa Arimathaya, mjumbe wa Baraza Kuu, aliyeheshimika sana. Yeye pia alikuwa anatazamia kuja kwa ufalme wa Mungu. Basi, alimwendea Pilato bila woga, akaomba apewe mwili wa Yesu. Pilato alishangaa kusikia kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa. Basi, akamwita jemadari, akamwuliza kama Yesu alikuwa amekufa kitambo. Pilato alipoarifiwa na huyo jemadari kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa, akamruhusu Yosefu kuuchukua mwili wake. Hapo Yosefu akanunua sanda ya kitani, akauteremsha chini huo mwili, akauzungushia sanda. Akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa mwambani, kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango. Nao Maria Magdalene na Maria mama yake Yose walipaona hapo alipolazwa. Baada ya siku ya Sabato, Maria Magdalene, Salome na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu. Basi, alfajiri na mapema siku ya Jumapili, walifika kaburini, jua lilipoanza kuchomoza. Nao wakawa wanaambiana, “Nani atakayetuondolea lile jiwe mlangoni mwa kaburi?” Lakini walipotazama, waliona jiwe limekwisha ondolewa. (Nalo lilikuwa kubwa mno.) Walipoingia kaburini, walimwona kijana mmoja aliyevaa vazi jeupe, ameketi upande wa kulia; wakashangaa sana. Lakini huyo kijana akawaambia, “Msishangae. Mnamtafuta Yesu wa Nazareti aliyesulubiwa. Amefufuka, hayumo hapa. Tazameni mahali walipokuwa wamemlaza. Nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro ya kwamba anawatangulieni kule Galilaya. Huko mtamwona kama alivyowaambieni.” Basi, wakatoka pale kaburini mbio, maana walitetemeka kwa hofu na kushangaa. Hawakumwambia mtu yeyote kitu, kwa sababu waliogopa mno. [ Yesu alipofufuka mapema Jumapili, alijionesha kwanza kwa Maria Magdalene, ambaye Yesu alikuwa amemtoa pepo wabaya saba. Maria Magdalene akaenda, akawajulisha wale waliokuwa pamoja na Yesu, na wakati huo walikuwa wanaomboleza na kulia. Lakini waliposikia ya kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria Magdalene amemwona, hawakuamini. Baadaye Yesu aliwatokea wanafunzi wawili akiwa na sura nyingine. Wanafunzi hao walikuwa wanakwenda shambani. Nao pia wakaenda, wakawaambia wenzao. Hata hivyo hawakuamini. Mwishowe Yesu aliwatokea wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa pamoja mezani. Akawakemea sana kwa sababu ya kutoamini kwao na ukaidi wao, maana hawakuwaamini wale waliokuwa wamemwona baada ya kufufuka. Basi, akawaambia, “Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu. Anayeamini na kubatizwa ataokolewa. Asiyeamini atahukumiwa. Na ishara hizi zitaandamana na wale wanaoamini: Kwa jina langu watatoa pepo na watasema kwa lugha mpya. Wakishika nyoka au wakinywa kitu chochote chenye sumu, hakitawadhuru. Watawawekea wagonjwa mikono, nao watapona.” Basi, Bwana Yesu alipokwisha sema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi upande wa kulia wa Mungu. Wanafunzi wakaenda wakihubiri kila mahali. Bwana akafanya kazi pamoja nao na kuimarisha ujumbe huo kwa ishara zilizoandamana nao. ] Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu. Waliyaandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona mambo hayo kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo. Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango, ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa. Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha ukuhani cha Abiya. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni. Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama. Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana. Siku moja, ilipokuwa zamu yake kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, Zakaria alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini malaika akamwambia, “Zakaria, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. Atakuwa mkubwa mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama ya Elia. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake.” Zakaria akamwambia huyo malaika, “Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu.” Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu; nimetumwa niseme nawe, nikuletee hizi habari njema. Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia.” Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakaria huku wakishangaa juu ya kukawia kwake hekaluni. Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu. Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani. Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: “Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu.” Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, kwa msichana mmoja bikira aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu, ewe uliyejaliwa neema na Mungu! Bwana yuko nawe!” Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: Maneno hayo yanamaanisha nini? Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu. Yeye atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?” Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.” Maria akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema.” Kisha yule malaika akaenda zake. Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yudea. Huko, aliingia katika nyumba ya Zakaria, akamsalimu Elisabeti. Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu, akasema kwa sauti kubwa, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa. Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? Nakuambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha. Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokuambia.” Naye Maria akasema, “Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu. Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri. Kwa kuwa Mungu Mwenye Nguvu amenifanyia makuu, jina lake ni takatifu. Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi. Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: Amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao; amewashusha wenye nguvu kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake, kama alivyowaahidia wazee wetu, Abrahamu na wazawa wake hata milele.” Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake. Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume. Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye. Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakaria. Lakini mama yake akasema, “Sivyo, bali ataitwa Yohane.” Wakamwambia, “Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?” Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani. Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: “Yohane ndilo jina lake.” Wote wakastaajabu. Papo hapo, midomo na ulimi wake Zakaria vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea. Wote waliosikia mambo hayo, waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: “Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye. Zakaria, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka unabii huu: “Atukuzwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amewajia na kuwakomboa watu wake. Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake. Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu, kwamba atatuokoa mikononi mwa maadui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia. Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu. Alimwapia Abrahamu babu yetu, kwamba atatujalia sisi tukombolewe mikononi mwa maadui zetu, tupate kumtumikia bila hofu, tuwe wanyofu na waadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu. Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake; kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao. Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atatuchomozea mwanga kutoka juu, na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani.” Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionesha rasmi kwa watu wa Israeli. Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote nchini kote wahesabiwe. Sensa hiyo ilikuwa mara ya kwanza, wakati Kurenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria. Basi, wote waliohusika walikwenda kuhesabiwa kila mtu katika mji wake. Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya, na kwa vile alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi, alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yudea, alikozaliwa mfalme Daudi. Alikwenda kuhesabiwa pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mjamzito. Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia, akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana. Malaika akawaambia, “Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kubwa itakayowapata watu wote. Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana. Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini.” Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema: “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu anaowafadhili!” Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: “Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha.” Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini. Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake. Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji. Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake. Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa. Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na sheria, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele za Bwana. Katika sheria ya Bwana imeandikwa: “Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana.” Pia walikwenda ili watoe sadaka: Hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika sheria ya Bwana. Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na sheria, Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu, akisema: “Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, umruhusu mtumishi wako aende kwa amani. Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu ulioleta, ambao umeutayarisha uonekane na watu wote: Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli.” Baba yake Yesu na mama yake walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto. Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu; na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako.” Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa. Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana. Saa hiyohiyo, alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na kueleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu. Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, wilayani Galilaya. Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa naye. Wazazi wake walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta. Siku ya tatu, walimkuta hekaluni kati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, “Mwanangu, kwa nini umetutendea hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni.” Yeye akawajibu, “Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia. Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu. Mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alikuwa anatawala mkoa wa Yudea. Herode alikuwa mtawala wa Galilaya, na ndugu yake Filipo alikuwa mtawala wa eneo la Iturea na Trakoniti. Lusania alikuwa mtawala wa Abilene, na Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Wakati huo ndipo neno la Mungu lilipomjia Yohane mwana wa Zakaria, kule jangwani. Basi, Yohane akaenda katika sehemu zote zilizopakana na mto Yordani. Akawa anahubiri watu watubu na kubatizwa ili Mungu awaondolee dhambi. Ndivyo ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake; nyosheni barabara zake. Kila bonde litafukiwa, kila mlima na kilima vitasawazishwa; palipopindika patanyoshwa, njia mbaya zitatengenezwa. Na, watu wote watauona wokovu aletao Mungu.’” Basi, Yohane akawa anawaambia watu wengi waliofika ili awabatize: “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea muikimbie ghadhabu inayokuja? Onesheni kwa vitendo kwamba mmetubu. Msianze sasa kujisemea: ‘Baba yetu ni Abrahamu!’ Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu. Basi, shoka liko tayari kwenye mizizi ya miti; hivyo kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.” Umati wa watu ukamwuliza, “Tufanye nini basi?” Akawajibu, “Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo.” Nao watozaushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, “Mwalimu, tufanye nini?” Naye akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa.” Nao askari wakamwuliza, “Na sisi tufanye nini?” Naye akawajibu, “Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu.” Wote walikuwa wanatazamia kitu fulani; basi, wakaanza kujiuliza mioyoni mwao kuhusu Yohane, kuwa labda yeye ndiye Kristo. Hapo Yohane akawaambia wote, “Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini anakuja mwenye uwezo kuliko mimi ambaye sistahili hata kumfungulia kamba za viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Yeye anacho mikononi mwake chombo cha kupuria nafaka aipure nafaka yake, akusanye ngano katika ghala, na makapi ayachome kwa moto usiozimika.” Hivyo, pamoja na mawaidha mengine mengi, Yohane aliwahimiza watu akiwahubiria Habari Njema. Lakini Yohane alimgombeza mtawala Herode, kwa sababu alikuwa amemchukua Herodia mke wa ndugu yake, na kumfanya mke wake; na pia kwa ajili ya mabaya yote aliyokuwa amefanya. Kisha Herode akazidisha ubaya wake kwa kumtia Yohane gerezani. Watu wote walipokuwa wamekwisha batizwa, Yesu naye alibatizwa. Na alipokuwa akisali, mbingu zilifunguka, na Roho Mtakatifu akamshukia akiwa na umbo kama la njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ndiwe Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.” Yesu alipoanza kazi yake hadharani alikuwa na umri upatao miaka thelathini, na watu walidhani yeye ni mtoto wa Yosefu mwana wa Heli. Heli alikuwa mwana wa Mathati, aliyekuwa mwana wa Lawi, mwana wa Melki, mwana wa Yanai, mwana wa Yosefu, aliyekuwa mwana wa Matathia, mwana wa Amosi, mwana wa Nahumu, mwana wa Hesli, mwana wa Nagai, aliyekuwa mwana wa Maathi, mwana wa Matathia, mwana wa Shemeni, mwana wa Yoseki, mwana wa Yuda, aliyekuwa mwana wa Yohanani, mwana wa Resa, mwana wa Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mwana wa Neri, mwana wa Melki, mwana wa Adi, mwana wa Kosamu, aliyekuwa mwana wa Elmadamu, mwana wa Eri, aliyekuwa mwana wa Yoshua, mwana wa Eliezeri, mwana wa Yorimu, mwana wa Mathati, mwana wa Lawi, aliyekuwa mwana wa Simeoni, mwana wa Yuda, mwana wa Yosefu, mwana wa Yonamu, mwana wa Eliakimu, aliyekuwa mwana wa Melea, mwana wa Mena, mwana wa Matatha, mwana wa Nathani, mwana wa Daudi, aliyekuwa mwana wa Yese, mwana wa Obedi, mwana wa Boazi, mwana wa Salmoni, mwana wa Nashoni, aliyekuwa mwana wa Aminadabu, mwana wa Admini, mwana wa Arni, mwana wa Hesroni, mwana wa Peresi, mwana wa Yuda, aliyekuwa mwana wa Yakobo, mwana wa Isaka, mwana wa Abrahamu, mwana wa Tera, mwana wa Nahori, aliyekuwa mwana wa Serugi, mwana wa Reu, mwana wa Pelegi, mwana wa Eberi, mwana wa Sala, aliyekuwa mwana wa Kainamu, mwana wa Arfaksadi, mwana wa Shemu, mwana wa Noa, mwana wa Lameki, aliyekuwa mwana wa Methusela, mwana wa Henoki, mwana wa Yaredi, mwana wa Mahalaleli, mwana wa Kainamu, aliyekuwa mwana wa Enoshi, mwana wa Sethi, mwana wa Adamu, aliyekuwa wa Mungu. Yesu alitoka mtoni Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani. Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa. Ndipo Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.” Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’” Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia, “Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza. Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu.” Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Utamwabudu Bwana Mungu wako, na kumtumikia yeye peke yake.’” Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa hekalu, akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini kwa maana imeandikwa: ‘Atawaamuru malaika wake wakulinde,’ na tena, ‘Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa mguu kwenye jiwe.’” Lakini Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’” Ibilisi alipokwisha mjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda. Hapo Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani. Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote. Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti. Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani ameniweka wakfu niwaletee maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka uhuru wao, na vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana.” Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho. Naye akaanza kuwaambia, “Andiko hili mlilosikia limetimia leo.” Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?” Naye akawaambia, “Bila shaka mtaniambia msemo huu: ‘Mganga jiponye mwenyewe,’ na pia mtasema: ‘Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye pia hapa kijijini mwako.’” Akaendelea kusema, “Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi kijijini mwake. Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Elia. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote. Hata hivyo, Elia hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarefathi katika Sidoni. Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani mwenyeji wa Siria.” Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana. Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini. Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake. Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu wilayani Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato. Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha. Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio: “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!” Yesu akamkemea huyo pepo akisema: “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo. Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, “Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!” Habari za Yesu zikaenea mahali pote katika eneo lile. Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye. Yesu akaja akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Yule mama akainuka mara, akawatumikia. Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote. Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walijua kwamba yeye ndiye Kristo. Kesho yake asubuhi, Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta. Hao watu walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao. Lakini yeye akawaambia, “Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo.” Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea. Siku moja, Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa Genesareti, na watu wengi walikuwa wamemzunguka wakisongamana, wanasikiliza neno la Mungu. Akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa. Wavuvi wenyewe walikuwa wametoka, wanaosha nyavu zao. Baada ya Yesu kuingia katika mashua moja iliyokuwa ya Simoni, alimtaka Simoni aisogeze majini, mbali kidogo na ukingo wa ziwa. Akaketi, akafundisha umati wa watu akiwa ndani ya mashua. Alipomaliza kufundisha, akamwambia Simoni, “Endesha mashua mpaka kilindini, mkatupe nyavu zenu mpate kuvua samaki.” Simoni akamjibu, “Bwana, tumejitahidi kuvua samaki usiku kucha bila kupata kitu, lakini kwa kuwa umesema, nitatupa nyavu.” Baada ya kufanya hivyo, wakavua samaki wengi, hata nyavu zao zikaanza kukatika. Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja, wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama. Simoni Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, “Ondoka mbele yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!” Simoni pamoja na wenzake wote walishangaa kwa kupata samaki wengi vile. Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu.” Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata. Ikawa, Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ya huko, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamwona. Basi, mtu huyo akaanguka kifudifudi akamwomba Yesu: “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.” Yesu akanyosha mkono, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika!” Mara ule ukoma ukamwacha. Naye Yesu akamwamuru: “Usimwambie mtu yeyote; bali nenda ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.” Lakini habari za Yesu zilizidi kuenea kila mahali. Watu makundi mengi wakakusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Lakini yeye alikwenda zake mahali pasipo na watu, akawa anasali huko. Siku moja, Yesu alikuwa akifundisha. Mafarisayo na waalimu wa sheria kutoka katika kila kijiji cha Galilaya, Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi hapo. Nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye kwa ajili ya kuponya wagonjwa. Mara watu wakaja, wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani; wakajaribu kumwingiza ndani, wamweke mbele ya Yesu. Lakini, kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya paa, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu. Yesu alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, “Rafiki, umesamehewa dhambi zako.” Waalimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: “Nani huyu anayesema maneno ya kufuru? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!” Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, “Mnawaza nini mioyoni mwenu? Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi,’ au kusema, ‘Simama utembee?’ Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Simama, chukua kitanda chako, uende zako nyumbani.” Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda nyumbani kwake huku akimtukuza Mungu. Wote wakashangaa na kushikwa na hofu; wakamtukuza Mungu wakisema: “Tumeona maajabu leo.” Baada ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtozaushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi ofisini. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Naye akaacha yote akamfuata. Lawi akamwandalia Yesu karamu kubwa nyumbani mwake. Na kundi kubwa la watozaushuru na watu wengine walikuwa wameketi pamoja nao. Mafarisayo na waalimu wa sheria wakawanungunikia wanafunzi wake wakisema: “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?” Yesu akawajibu, “Wenye afya hawamhitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi, wapate kutubu.” Watu wengine wakamwambia, “Wafuasi wa Yohane Mbatizaji hufunga mara kwa mara na kusali; hata wafuasi wa Mafarisayo hufanya vivyo hivyo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa.” Yesu akawajibu, “Je, wale walioalikwa harusini hutakiwa wafunge hali bwana arusi yuko pamoja nao? La! Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.” Yesu akawaambia mfano huu: “Watu hawakati kiraka cha nguo mpya na kukitia katika vazi kuukuu; kama wakifanya hivyo, watakuwa wamelikata hilo vazi jipya, na pia hicho kiraka hakitachukuana na hilo vazi kuukuu. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; kwani hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, divai itamwagika, na viriba vitaharibika. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya. Hakuna mtu anayetamani kunywa divai mpya baada ya kunywa divai ya zamani kwani husema ‘Ile ya zamani ni nzuri zaidi.’” Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala. Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Haikuruhusiwa mtu kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani.” Hivyo akawaambia, “Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.” Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani kulikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kulia ulikuwa umepooza. Waalimu wa sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisa cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato. Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka, simama katikati.” Yule mtu akaenda kusimama katikati. Kisha Yesu akawaambia, “Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?” Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena. Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu. Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali. Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo, Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote), Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti. Baada ya kushuka mlimani pamoja nao, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao. Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote. Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema: “Heri nyinyi mlio maskini, maana ufalme wa Mungu ni wenu. Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri nyinyi mnaolia sasa, maana baadaye mtacheka kwa furaha. “Heri yenu nyinyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu. Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo. Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri, maana mmekwisha pata faraja yenu. Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa, maana baadaye mtasikia njaa. Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa, maana baadaye mtaomboleza na kulia. Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu, maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo. “Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako. Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie. Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. “Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao. Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo. Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile. Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya. Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma. “Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa. Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.” Akawaambia mfano huu: “Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni. Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake. Kwa nini wakiona kibanzi jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ na huku huioni boriti iliyomo katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyomko jichoni mwako, na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako. “Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili. Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake. “Mbona mwaniita ‘Bwana, Bwana,’ na huku hamtimizi yale ninayosema? Nitawapeni mfano unaofaa kuonesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza: Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara. Lakini yeyote anayesikia maneno yangu asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!” Baada ya kusema yale aliyotaka watu wasikie, Yesu alikwenda Kafarnaumu. Huko kulikuwa na jemadari mmoja ambaye alikuwa na mtumishi wake aliyempenda sana. Huyu mtumishi alikuwa mgonjwa karibu na kufa. Yule jemadari aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee fulani Wayahudi waende kumwomba aje kumponya mtumishi wake. Walipofika kwa Yesu, walimsihi sana, wakasema: “Huyu anastahili afanyiwe jambo hilo, kwa maana yeye analipenda taifa letu, na ndiye aliyetujengea lile sunagogi.” Basi, Yesu akaenda pamoja nao. Alipokuwa karibu na kufika nyumbani kwa yule jemadari, yule jemadari aliwatuma marafiki zake wamwambie Yesu: “Bwana, usijisumbue zaidi, maana mimi sistahili uingie nyumbani mwangu. Ndio maana sikujiona nastahili hata kuja kwako. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi pia ni mtu niliye chini ya mamlaka, na ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; namwambia mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.” Yesu aliposikia hayo, alishangaa, halafu akauelekea ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akasema, “Sijaona mwenye imani kama hii hata katika Israeli!” Wale watu walipowasili nyumbani walimkuta yule mtumishi hajambo kabisa. Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja uitwao Naini, na wafuasi wake na kundi kubwa la watu waliandamana naye. Basi, alipokuwa anakaribia lango la mji, walitokea watu wamebeba maiti ya mwanamume mmoja, mtoto wa pekee wa mama mjane. Watu wengi wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mama. Bwana alipomwona mama huyo akamwonea huruma, akamwambia, “Usilie.” Kisha, akaenda akaligusa lile jeneza, na wale waliokuwa wamelichukua wakasimama. Halafu akasema, “Kijana! Nakuamuru, amka!” Yule aliyekufa akaketi, akaanza kuongea. Na Yesu akamkabidhi kwa mama yake. Watu wote walishikwa na hofu, wakawa wanamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea kati yetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.” Habari hizo zikaenea kote katika Yudea na katika nchi za jirani. Wanafunzi wa Yohane walimhabarisha Yohane juu ya mambo hayo yote. Naye Yohane, baada ya kuwaita wawili kati ya wanafunzi wake, aliwatuma kwa Bwana wamwulize: “Wewe ndiye yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Wale wanafunzi walipomfikia Yesu wakamwambia, “Yohane Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: ‘Wewe ndiye yule anayekuja, au tumngoje mwingine?’” Wakati huohuo, Yesu alikuwa anawaponya watu wengi waliokuwa wanateseka kwa magonjwa na waliopagawa na pepo wabaya na kuwawezesha vipofu wengi kuona. Basi, Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane yale mliyojionea na kuyasikia: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami!” Hapo wajumbe wa Yohane walipokwisha kwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu juu ya Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo? Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Wanaovaa mavazi maridadi na kuishi maisha ya anasa, hukaa katika majumba ya wafalme! Basi, niambieni, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii. Huyu Yohane ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Tazama mimi namtuma mtumishi wangu akutangulie; ambaye atakutayarishia njia yako.’” Yesu akamalizia kwa kusema, “Nawaambieni, kati ya binadamu wote hakuna aliye mkubwa zaidi kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkubwa kuliko yeye.” Waliposikia hayo watu wote na watozaushuru waliusifu wema wa Mungu; hao ndio wale waliokuwa wameupokea ubatizo wa Yohane. Lakini Mafarisayo na waalimu wa sheria walikataa mpango wa Mungu uliowahusu, wakakataa kubatizwa na Yohane. Yesu akaendelea kusema, “Basi, nitawafananisha watu wa kizazi hiki na kitu gani? Ni watu wa namna gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa sokoni na kuambiana, kikundi kimoja na kingine: ‘Tumewapigieni ngoma, lakini hamkucheza! Tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkulia!’ Kwa maana Yohane alikuja, akawa anafunga na hakunywa divai, nanyi mkasema: ‘Amepagawa na pepo!’ Naye Mwana wa Mtu amekuja, anakula na kunywa, nanyi mkasema: ‘Mwangalieni mlafi huyu na mlevi; rafiki ya watozaushuru na wenye dhambi!’ Hata hivyo, hekima ya Mungu imethibitishwa kuwa njema na wote wale wanaoikubali.” Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani kwake. Akaingia nyumbani kwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula. Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja mwenye dhambi. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi. Akaja, akasimama karibu na miguu yake Yesu, akilia, na machozi yake yakamdondokea Yesu miguuni. Huyo mwanamke akaipangusa miguu ya Yesu kwa nywele zake. Kisha akaibusu na kuipaka yale marashi. Yule Mfarisayo aliyemwalika Yesu alipoona hayo, akawaza moyoni mwake, “Kama mtu huyu angekuwa kweli nabii angejua huyu mwanamke ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.” Yesu akamwambia huyo Mfarisayo, “Simoni, ninacho kitu cha kukuambia.” Naye Simoni akamwambia, “Ndio Mwalimu, sema.” Yesu akasema, “Watu wawili walikuwa wamemkopa mtu fedha: Mmoja alikuwa amekopa denari 500, na mwingine hamsini. Waliposhindwa kulipa madeni yao, huyo mtu aliwasamehe wote wawili. Sasa ni yupi kati ya hao wawili atampenda zaidi huyo bwana?” Simoni akamjibu, “Ni dhahiri kwamba yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi atampenda zaidi yule bwana.” Yesu akamwambia, “Sawa.” Halafu akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, “Unamwona huyu mwanamke, sivyo? Basi, mimi nilipoingia hapa nyumbani kwako hukunipa maji ya kunawa miguu yangu; lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kunipangusa kwa nywele zake. Wewe hukunisalimu kwa kunibusu, lakini huyu mwanamke tangu nilipoingia hapa amekuwa akiibusu miguu yangu. Wewe hukunionesha ukarimu wako kwa kunipaka mafuta kichwani, lakini huyu mwanamke amefanya hivyo kwa kunipaka mafuta miguu yangu. Kwa hiyo nakuambia amesamehewa dhambi zake nyingi kwa kuwa ameonesha upendo mkubwa. Mwenye kusamehewa kidogo, hupenda kidogo.” Basi, Yesu akamwambia yule mwanamke, “Umesamehewa dhambi zako.” Ndipo wale waliokuwa pamoja naye mezani wakaulizana, “Ni mtu wa namna gani huyu awezaye kusamehe dhambi?” Naye Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.” Baada ya hayo, Yesu alipitia mijini na vijijini akitangaza Habari Njema za ufalme wa Mungu. Wale kumi na wawili waliandamana naye. Pia wanawake kadhaa ambao Yesu alikuwa amewatoa pepo wabaya na kuwaponya magonjwa, waliandamana naye. Hao ndio akina Maria (aitwaye Magdalene), ambaye alitolewa pepo wabaya saba; Yoana mke wa Kuza, mfanyakazi mkuu wa Herode; Susana na wengine kadhaa. Hao wanawake walikuwa wakiwatumikia kwa mali yao wenyewe. Wakati mmoja kundi kubwa la watu lilikuwa linakusanyika, na watu walikuwa wanamjia Yesu kutoka kila mji. Naye akawaambia mfano huu: “Mpanzi alikwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akipanda hizo mbegu, nyingine zilianguka njiani, na wapita njia wakazikanyaga na ndege wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe, na baada ya kuota zikanyauka kwa kukosa maji. Nyingine zilianguka kati ya miti ya miiba. Ile miti ya miiba ilipoota ikazisonga. Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikaota na kuzaa asilimia mia.” Baada ya kusema hayo, akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio na asikie!” Wanafunzi wake Yesu wakamwuliza maana ya mfano huo. Naye akajibu, “Nyinyi mmejaliwa kujua siri za ufalme wa Mungu, lakini hao wengine sivyo; ila hao huambiwa kwa mifano, ili wakitazama wasiweze kuona, na wakisikia wasifahamu. “Basi, maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu. Zile zilizoanguka njiani zinaonesha watu wale wanaosikia lile neno, halafu Ibilisi akaja na kuliondoa mioyoni mwao wasije wakaamini wakaokoka. Zile zilizoanguka penye mawe zinaonesha watu wale ambao wanaposikia juu ya lile neno hulipokea kwa furaha. Lakini kama zile mbegu, watu hao hawana mizizi maana husadiki kwa kitambo tu, na wanapojaribiwa hukata tamaa. Zile zilizoanguka kwenye miti ya miiba ni watu wale wanaosikia lile neno, lakini muda si muda, wanapokwenda zao, husongwa na wasiwasi, mali na anasa za maisha, nao hawazai matunda yakakomaa. Na zile zilizoanguka kwenye udongo mzuri ndio watu wale wanaolisikia lile neno, wakalizingatia kwa moyo mwema na wa utii. Hao huvumilia mpaka wakazaa matunda. “Watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe au kuiweka mvunguni. Lakini huiweka juu ya kinara ili watu wanapoingia ndani wapate kuona mwanga. “Chochote kilichofichwa kitafichuliwa, na siri yoyote itagunduliwa na kujulikana hadharani. “Kwa hiyo, jihadharini jinsi mnavyosikia; maana aliye na kitu ataongezewa, lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho, kitachukuliwa.” Hapo mama na ndugu zake Yesu wakamjia, lakini hawakuweza kumkaribia kwa sababu ya umati wa watu. Yesu akapewa habari kwamba mama na ndugu zake walikuwa nje, wanataka kumwona. Lakini Yesu akawaambia watu wote, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.” Siku moja, Yesu alipanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvuke ziwa twende mpaka ngambo.” Basi, wakaanza safari. Walipokuwa wanasafiri kwa mashua, Yesu alishikwa na usingizi, akalala. Dhoruba kali ikaanza kuvuma, maji yakaanza kuingia ndani ya mashua, wakawa katika hatari. Wale wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwamsha wakisema, “Bwana, Bwana! Tunaangamia!” Yesu akaamka, akaukemea upepo na mawimbi ya maji, navyo vikatulia, kukawa shwari. Kisha akawaambia, “Iko wapi imani yenu?” Lakini wao walishangaa na kuogopa huku wakiambiana, “Huyu ni nani basi, hata anaamuru dhoruba na mawimbi, navyo vinamtii?” Wakaendelea na safari, wakafika pwani ya nchi ya Wagerase inayokabiliana na Galilaya, ngambo ya ziwa. Alipokuwa anashuka pwani, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo alimjia kutoka mjini. Kwa muda mrefu mtu huyo hakuwa anavaa nguo, wala hakuwa anaishi nyumbani bali makaburini. Alipomwona Yesu, alijitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kubwa, “We, Yesu Mwana wa Mungu Mkuu, una shauri gani nami? Ninakusihi usinitese!” Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia huyo pepo mchafu amtoke mtu huyo. Pepo huyo mchafu alikuwa anamvamia mtu huyo mara nyingi, na ingawa watu walimweka ndani na kumfunga kwa minyororo na pingu, lakini kila mara alivivunja vifungo hivyo, akakimbizwa na pepo huyo mchafu hadi jangwani. Basi, Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?” Yeye akajibu, “Jina langu ni ‘Jeshi’” — kwa sababu pepo wengi walikuwa wamempagaa. Hao pepo wakamsihi asiwapeleke kwenye shimo kuu. Mahali hapo kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha mlimani. Basi, hao pepo wakamsihi awaruhusu wawaingie. Naye Yesu akawapa ruhusa. Kwa hiyo pepo hao wakamtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nao wakaporomoka kwenye ule mteremko mkali, wakatumbukia ziwani, wakafa maji. Wale wachungaji walipoona yote yaliyotokea walikimbia, wakaenda kuwapa watu habari mjini na mashambani. Watu wakaja kuona yaliyotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mtu aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, ana akili zake, wakaogopa. Wale watu walioshuhudia tukio hilo waliwaeleza hao jinsi yule mtu alivyoponywa. Wakazi wa nchi ya Gerase walishikwa na hofu kubwa. Kwa hiyo wakamwomba Yesu aondoke, aende zake. Hivyo Yesu alipanda tena mashua, akaondoka. Yule mtu aliyetokwa na wale pepo akamsihi aende pamoja naye. Lakini Yesu hakumruhusu, bali akamwambia, “Rudi nyumbani ukaeleze yote Mungu aliyokutendea.” Basi, yule mtu akaenda akitangaza kila mahali katika mji ule mambo yote Yesu aliyomtendea. Yesu aliporudi upande mwingine wa ziwa, kundi la watu lilimkaribisha, kwa maana wote walikuwa wanamngojea. Hapo akaja mtu mmoja aitwaye Yairo, ofisa wa sunagogi. Alijitupa miguuni pa Yesu, akamwomba aende nyumbani kwake, kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa. Yesu alipokuwa akienda, watu wakawa wanamsonga kila upande. Basi, kulikuwa na mwanamke mmoja kati ya lile kundi la watu, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili; ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote kwa waganga, hakuna aliyefaulu kumponya. Huyo mwanamke alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. Papo hapo akaponywa ugonjwa wake wa kutokwa damu. Yesu akasema, “Ni nani aliyenigusa?” Wote wakasema kwamba hapakuwa na mtu aliyemgusa. Naye Petro akasema, “Bwana, umati wa watu umekuzunguka na kukusonga!” Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, maana nimehisi nguvu imenitoka.” Yule mwanamke alipoona kwamba hawezi kujificha, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa mbele ya Yesu. Hapo akaeleza mbele ya wote kisa cha kumgusa Yesu na jinsi alivyoponywa mara moja. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda na amani.” Alipokuwa bado akiongea, Yairo akaletewa habari kutoka nyumbani: “Binti yako amekwisha kufa, ya nini kumsumbua Mwalimu zaidi?” Yesu aliposikia hayo akamwambia Yairo, “Usiogope; amini tu, naye atapona.” Alipofika nyumbani hakumruhusu mtu kuingia ndani pamoja naye, isipokuwa Petro, Yohane, Yakobo na wazazi wa huyo msichana. Watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili yake. Lakini Yesu akawaambia, “Msilie, kwa maana mtoto hajafa, amelala tu!” Nao wakamcheka kwa sababu walijua kwamba alikuwa amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono akasema, “Mtoto, amka!” Roho yake ikamrudia, akaamka mara. Yesu akaamuru wampe chakula. Wazazi wake walishangaa, lakini Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote hayo yaliyotendeka. Yesu aliwaita wale kumi na wawili, akawapa uwezo wa kuponya pepo wote, na uwezo wa kuponya wagonjwa. Halafu akawatuma waende kuhubiri ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. Akawaambia, “Mnaposafiri msichukue chochote: Msichukue fimbo, wala mkoba, wala chakula, wala fedha, wala hata koti la ziada. Nyumba yoyote mtakayoingia na kukaribishwa, kaeni humo mpaka mtakapoondoka katika kijiji hicho. Watu wakikataa kuwakaribisha, tokeni katika mji huo, nanyi mnapotoka kunguteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.” Basi, wakaanza safari, wakapitia vijijini wakihubiri Habari Njema na kuponya wagonjwa kila mahali. Sasa, mtawala Herode alipata habari za mambo yote yaliyokuwa yanatendeka, akawa na wasiwasi kwa vile walikuwa wakisema: “Yohane amefufuka kutoka kwa wafu!” Wengine walisema kwamba Elia ametokea, na wengine walisema kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amerudi duniani. Lakini Herode akasema, “Huyo Yohane nilimkata kichwa; sasa ni nani huyu ninayesikia habari zake?” Akawa na hamu ya kumwona. Wale mitume waliporudi, walimweleza Yesu yote waliyoyafanya. Yesu akawachukua, wakaenda peke yao mjini Bethsaida. Lakini wale watu walipojua alikokwenda, walimfuata. Yesu akawakaribisha akawazungumzia juu ya ufalme wa Mungu, akawaponya wale waliohitaji kuponywa. Jua lilipokuwa linaanza kutua, wale kumi na wawili walimwendea wakamwambia, “Waage watu waende kwenye vijiji na mashamba ya karibu, wakajipatie chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tulipo ni nyikani.” Lakini Yesu akawaambia, “Wapeni nyinyi chakula.” Wakamjibu, “Hatuna chochote ila mikate mitano na samaki wawili. Labda twende wenyewe tukawanunulie chakula watu wote hawa!” (Walikuwapo pale wanaume wapatao 5,000.) Basi, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Waambieni watu waketi katika makundi ya watu hamsinihamsini.” Wanafunzi wakafanya walivyoambiwa, wakawaketisha wote. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. Watu wote wakala, wakashiba. Wakakusanya mabaki ya chakula, wakajaza vikapu kumi na viwili. Siku moja, Yesu alikuwa anasali peke yake, na wanafunzi wake walikuwa karibu. Basi, akawauliza, “Watu wanasema mimi ni nani?” Nao wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa wewe ni Yohane Mbatizaji; wengine, Elia; wengine, mmojawapo wa manabii wa kale ambaye amefufuka.” Hapo akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo wa Mungu.” Halafu Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hiyo. Akaendelea kusema kwamba ni lazima Mwana wa Mtu apate mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria na kuuawa, lakini siku ya tatu atafufuliwa. Kisha akawaambia watu wote, “Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate. Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayaokoa. Je, kuna faida gani mtu kuupata utajiri wote wa dunia kwa kujipoteza au kujiangamiza yeye mwenyewe? Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu. Nawaambieni kweli, kuna wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu.” Yapata siku nane baada ya kusema hayo, Yesu aliwachukua Petro, Yohane na Yakobo, akaenda nao mlimani kusali. Alipokuwa akisali, sura yake ilibadilika, mavazi yake yakawa meupe na kungaa sana. Na watu wawili wakaonekana wakizungumza naye, nao walikuwa Mose na Elia, ambao walitokea wakiwa wenye utukufu, wakazungumza naye juu ya kutoka kwake ambako angekamilisha huko Yerusalemu. Petro na wenzake walikuwa wamelemewa na usingizi mzito, hata hivyo waliamka, wakauona utukufu wake, wakawaona na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. Basi, watu hao wawili walipokuwa wakiondoka, Petro alimwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa! Basi, tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” Kwa kweli hakujua anasema nini. Petro alipokuwa akisema hayo, mara wingu likatokea na kuwafunika; na wingu hilo lilipowajia, wale wanafunzi waliogopa sana. Sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu: “Huyu ndiye Mwanangu niliyemchagua, msikilizeni.” Baada ya hiyo sauti kusikika, Yesu alionekana akiwa peke yake. Wanafunzi walikaa kimya juu ya tukio hilo, na wakati ule hawakumwambia mtu yeyote mambo hayo waliyoyaona. Kesho yake walipokuwa wakishuka kule mlimani, kundi kubwa la watu lilikutana na Yesu. Hapo, mtu mmoja katika lile kundi akapaza sauti, akasema, “Mwalimu! Ninakusihi umwangalie mwanangu-mwanangu wa pekee! Pepo huwa anamshambulia, na mara humfanya apige kelele; humtia kifafa, na povu likamtoka kinywani. Huendelea kumtesa sana, asimwache upesi. Niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze, lakini hawakuweza.” Yesu akasema, “Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini?” Kisha akamwambia huyo mtu, “Mlete mtoto wako hapa.” Wakati mtoto huyo alipokuwa anamjia Yesu, yule pepo alimwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu akamponya mtoto na kumkabidhi kwa baba yake. Watu wote wakashangazwa na uwezo mkuu wa Mungu. Wale watu walipokuwa bado wanashangaa juu ya mambo yote aliyofanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Tegeni masikio, muyasikie mambo haya: Mwana wa Mtu anakwenda kutiwa mikononi mwa watu.” Lakini wao hawakuelewa maana ya usemi huo. Jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao ili wasitambue; nao wakaogopa kumwuliza juu ya msemo huo. Kukatokea majadiliano kati ya wale wanafunzi kuhusu nani kati yao aliyekuwa mkuu zaidi. Yesu aliyajua mawazo yaliyokuwa mioyoni mwao; basi akamchukua mtoto mdogo akamweka karibu naye, akawaambia, “Mtu yeyote anayempokea mtoto huyu mdogo kwa jina langu, ananipokea mimi; na yeyote anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. Maana yule aliye mdogo kuliko wote kati yenu ndiye aliye mkuu kuliko wote.” Yohane alidakia na kusema, “Bwana, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu.” Lakini Yesu akamwambia, “Msimkataze; kwani asiyepingana nanyi yuko upande wenu.” Wakati ulipokaribia ambapo Yesu angechukuliwa juu mbinguni, yeye alikata shauri kwenda Yerusalemu. Basi, akawatuma wajumbe wamtangulie, nao wakaenda wakaingia kijiji kimoja cha Wasamaria ili wamtayarishie mahali. Lakini wenyeji wa hapo hawakutaka kumpokea kwa sababu alikuwa anaelekea Yerusalemu. Basi, wanafunzi wake, kina Yohane na Yakobo, walipoona hayo, wakasema, “Bwana, wataka tuamuru moto ushuke kutoka mbinguni uwateketeze?” Lakini yeye akawageukia, akawakemea. Wakatoka, wakaenda kijiji kingine. Walipokuwa wakisafiri njiani, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata kokote utakakokwenda.” Yesu akasema, “Mbweha wana mapango, na ndege wana viota lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia.” Kisha akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.” Lakini huyo akasema, “Bwana, niruhusu kwanza niende kumzika baba yangu.” Yesu akamwambia, “Waache wafu wazike wafu wao; bali wewe nenda ukatangaze ufalme wa Mungu.” Na mtu mwingine akamwambia, “Nitakufuata, lakini niruhusu kwanza nikawaage wale walio nyumbani kwangu.” Yesu akamwambia, “Yeyote anayeshika jembe tayari kulima na huku anaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.” Baada ya hayo, Bwana aliwachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawiliwawili, wamtangulie katika kila kijiji na mahali ambapo yeye mwenyewe alitaka kwenda. Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache. Kwa hivyo, mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake. Sasa nendeni; fahamuni kwamba ninawatuma nyinyi kama kondoo wanaokwenda kati ya mbwamwitu. Msichukue mfuko wa fedha, mkoba, wala viatu; msimsalimu mtu yeyote njiani. Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza wasalimuni hivi: ‘Amani iwe katika nyumba hii!’ Kama akiwako mpenda amani, amani yenu itakaa naye, la sivyo, itawarudieni. Kaeni katika nyumba hiyo mkila na kunywa wanavyowapeni, maana mfanyakazi anastahili mshahara wake. Msiende mara nyumba hii mara nyumba ile. Kama mkifika mji fulani na watu wakiwakaribisha, kuleni wanavyowapeni. Ponyeni wagonjwa walioko huko, waambieni watu: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia kwenu.’ Lakini mkiingia katika mji wowote, wasipowakaribisheni, tokeni; nanyi mpitapo katika barabara zao semeni: ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu tunayapangusa dhidi yenu. Lakini, jueni kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.’ Hakika nawaambieni, siku ile mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile ya watu wa Sodoma. “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kukaa katika majivu kutubu. Hata hivyo, siku ya hukumu nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni. Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu.” Halafu akasema, “Anayewasikiliza nyinyi, ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea nyinyi, anakataa kunipokea mimi. Na yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma.” Baadaye, wale sabini na wawili walirudi wamejaa furaha, wakisema, “Bwana, hata pepo wametutii tulipolitaja jina lako.” Yeye akawaambia, “Nilimwona Shetani jinsi alivyokuwa anaporomoka kama umeme kutoka mbinguni. Naam, nimewapeni uwezo wa kukanyaga nyoka na nge, na uwezo juu ya nguvu zote za yule adui; hakuna chochote kitakachowadhuru. Hata hivyo, msifurahi kwa sababu pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” Saa ileile, Yesu akafurahi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akasema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafumbulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza.” Kisha akasema, “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumfunulia.” Halafu akawaelekea wafuasi wake akawaambia, “Heri wanaoona yale mnayoyaona nyinyi! Hakika, manabii na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona nyinyi wasiyaone, na kusikia yale mnayoyasikia wasiyasikie.” Baadaye mwanasheria mmoja alisimama, akamwuliza akitaka kumtega, “Mwalimu, nifanye nini ili nipate uhai wa milele?” Yeye akamwuliza, “Imeandikwa nini katika sheria? Unaelewaje?” Akamjibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Yesu akamwambia, “Vema! Fanya hivyo, nawe utaishi.” Lakini yeye akitaka kujihakikishia kuwa mwema akamwuliza Yesu, “Na jirani yangu ni nani?” Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anashuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Alipokuwa njiani, alivamiwa na majambazi, wakamnyanganya mali yake na kumpiga, wakamwacha amelala pale nusu mfu. Kumbe, kuhani mmoja akawa anapita barabara ileile, akamwona, akapita kando. Hali kadhalika na Mlawi mmoja, alipofika mahali hapo akamwona, akapita kando. Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri, alifika pale yule mtu alipokuwa, naye alipomwona, alimwonea huruma. Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na divai na kuyafunga; halafu akampandisha juu ya punda wake, akampeleka katika nyumba moja ya wageni akamwuguza. Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye nyumba, akamwambia, ‘Mwuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi, nitakulipa nitakaporudi.’” Kisha Yesu akauliza, “Kati ya hao watatu, ni yupi aliyeonesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?” Yule mwalimu wa sheria akamjibu, “Ni yule aliyemwonea huruma.” Yesu akamwambia, “Nenda ukafanye vivyo hivyo.” Walipokuwa safarini, waliingia katika kijiji kimoja na mwanamke mmoja aitwaye Martha, akamkaribisha nyumbani kwake. Martha alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake. Lakini Martha alikuwa anashughulika na mambo mengi. Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, “Bwana, hivi hujali kwamba dada yangu ameniacha nishughulike peke yangu? Mwambie basi, anisaidie.” Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, unahangaika na kusumbuka kwa mambo mengi. Kitu kimoja tu ni muhimu. Maria amechagua kitu bora zaidi ambacho hakuna mtu atakayemnyanganya.” Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akisali. Alipomaliza kusali, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, tunakuomba utufundishe kusali kama Yohane Mbatizaji alivyowafundisha wanafunzi wake.” Yesu akawaambia, “Mnaposali, semeni: ‘Baba! Jina lako litukuzwe; ufalme wako ufike. Utupe daima chakula chetu cha kila siku. Utusamehe dhambi zetu, maana sisi tunawasamehe wote waliotukosea; wala usitutie katika majaribu.’” Kisha akawaambia, “Tuseme mmoja wenu anaye rafiki, akaenda kwake usiku wa manane, akamwambia: ‘Rafiki, tafadhali niazime mikate mitatu, kwa kuwa rafiki yangu amepitia kwangu akiwa safarini nami sina cha kumpa.’ Naye, akiwa ndani angemjibu: ‘Usinisumbue! Nimekwisha funga mlango. Mimi na watoto wangu tumelala; siwezi kuamka nikupe!’ Hakika, ingawa hataamka ampe kwa sababu yeye ni rafiki yake, lakini, kwa sababu ya huyo mtu kuendelea kumwomba, ataamka ampe chochote anachohitaji. Kwa hiyo, ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni mlango nanyi mtafunguliwa. Maana yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata na abishaye mlango hufunguliwa. Mtoto akimwomba baba yake samaki, je, atampa nyoka badala ya samaki? Na kama akimwomba yai, je, atampa nge? Kama nyinyi, ingawa ni waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi; atawapa Roho Mtakatifu wale wanaomwomba.” Siku moja Yesu alikuwa anamfukuza pepo aliyemfanya mtu mmoja kuwa bubu. Basi, huyo pepo alipomtoka, yule mtu akaweza kuongea, hata umati wa watu ukashangaa. Lakini baadhi ya watu hao wakasema, “Anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” Wengine, wakimjaribu, wakamtaka afanye ishara kuonesha kama alikuwa na idhini kutoka mbinguni. Lakini yeye, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika vikundi vinavyopingana hauwezi kudumu; kadhalika, jamaa yoyote iliyo na mafarakano huangamia. Kama Shetani anajipinga mwenyewe, utawala wake utasimamaje? Mnasemaje, basi, kwamba ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli? Kama ninafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, wafuasi wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo, wao ndio watakaowahukumu nyinyi. Lakini ikiwa ninafukuza pepo kwa uwezo wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. “Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama. Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara. Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya. “Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika. Asipopata, hujisemea: ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.’ Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa. Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba wabaya kuliko yeye; wote huenda, wakamwingia mtu huyo. Hivyo, hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko hapo mwanzo.” Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: “Heri mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!” Lakini Yesu akasema, “Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.” Umati wa watu ulipozidi kuongezeka, Yesu akawaambia, “Kizazi hiki ni kizazi kiovu. Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya Yona. Jinsi Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninewi, ndivyo pia Mwana wa Mtu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki. Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni na kumbe hapa pana mkuu kuliko Solomoni. Watu wa Ninewi watatokea wakati wa hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona; na kumbe hapa pana kikuu kuliko Yona! “Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa debe, bali huiweka juu ya kinara ili watu wanaoingia ndani wapate kuona mwanga. Jicho lako ni taa ya mwili wako; likiwa zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Jicho lako likiwa bovu, na mwili wako pia utakuwa katika giza. Uwe mwangalifu basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza. Basi, kama mwili wako wote una mwanga, bila kuwa na sehemu yoyote yenye giza, mwili huo utangaa kikamilifu kama vile taa inavyokuangazia kwa mwanga wake.” Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula. Huyo Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa kwanza. Bwana akamwambia, “Nyinyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa udhalimu na uovu. Wapumbavu nyinyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani pia? Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo ndani, na vingine vyote vitakuwa halali kwenu. “Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine, na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine. “Ole wenu nyinyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima hadharani. Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika; watu hutembea juu yake bila kufahamu.” Mmoja wa waalimu wa sheria akamwambia, “Mwalimu, maneno yako yanatukashifu na sisi pia.” Yesu akamjibu, “Na nyinyi waalimu wa sheria, ole wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku nyinyi wenyewe hamnyoshi hata kidole kuwasaidia. Ole wenu, kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii wale ambao wazee wenu waliwaua. Kwa hiyo mnashuhudia na kukubaliana na matendo ya wazee wenu; maana wao waliwaua hao manabii, nanyi mnajenga makaburi yao. Kwa hiyo, Hekima ya Mungu ilisema hivi: ‘Nitawapelekea manabii na mitume, lakini watawaua baadhi yao, na kuwatesa wengine.’ Matokeo yake ni kwamba kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu ya damu ya manabii wote iliyomwagika tangu mwanzo wa ulimwengu; tangu kumwagwa damu ya Abeli mpaka ile ya Zekaria ambaye walimuua kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, hakika kizazi hiki kitaadhibiwa kwa matendo hayo. “Ole wenu nyinyi waalimu wa sheria, kwa sababu mmeuficha ule ufunguo wa mlango wa elimu; nyinyi wenyewe hamkuingia na mmewazuia waliokuwa wanaingia wasiingie.” Alipokuwa akitoka pale, wale Mafarisayo na waalimu wa sheria walianza kumshambulia vikali na kumsonga kwa maswali mengi ili wapate kumnasa kwa maneno yake. Wakati watu kwa maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila kilichofichika kitafichuliwa. Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika mwanga, na kila mliyonongona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya nyumba. “Nawaambieni nyinyi rafiki zangu: Msiwaogope wale wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi. Nitawaonesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo. Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa sarafu ndogo kumi, au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope, basi; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi! “Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu kwamba mtu huyo ni wake. Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. “Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. “Watakapowapeleka nyinyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala, msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema. Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema.” Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba.” Yesu akamjibu, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au msuluhishi kati yenu?” Basi, akawaambia wote, “Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uhai wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo.” Kisha akawaambia mfano: “Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi. Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: ‘Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu? Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, nami nitahifadhi humo mavuno yangu yote na mali yangu. Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: Sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, kula, kunywa na kufurahi.’ Lakini Mungu akamwambia: ‘Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojirundikia vitakuwa vya nani?’” Yesu akamaliza kwa kusema, “Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejirundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu.” Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi. Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege! Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza kidogo urefu wa maisha yake? Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine? Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba! “Basi, msivurugike akili, mkihangaika juu ya mtakachokula au mtakachokunywa. Kwa maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wote wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo. Shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu, na hayo mtapewa kwa ziada. “Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni ufalme. Uzeni mali yenu mkawape maskini hizo fedha. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na kujiwekea hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu. Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako. “Muwe tayari mmejifunga mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka; muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka harusini, ili wamfungulie mara atakapobisha. Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia. Hata kama atarudi usiku wa manane au alfajiri na kuwakuta wanakesha, heri yao watumishi hao! Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.” Petro akamwambia, “Bwana, mfano huo ni kwa ajili yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?” Bwana akajibu, “Ni nani, basi, aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watumishi wake ili awape chakula wakati ufaao? Heri yake mtumishi huyo ikiwa bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. Hakika atampa madaraka juu ya mali yake yote. Lakini, kama mtumishi huyo akijisemea moyoni: ‘Bwana wangu amekawia sana kurudi;’ kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, wa kiume au wa kike, na kula, kunywa na kulewa, bwana wake atarudi siku asiyoitazamia na saa asiyoijua; atamwadhibu mtumishi huyo vibaya na kumweka fungu moja na wasioamini. Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana. Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atadaiwa vingi; aliyepewa vingi zaidi atadaiwa vingi zaidi. “Nimekuja kuwasha moto duniani; laiti ungekuwa umewaka tayari! Ninao ubatizo ambao inanipasa niupokee; jinsi gani ninavyohangaika mpaka ukamilike! Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo; si amani bali utengano. Na tangu sasa, jamaa ya watu watano itagawanyika; watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu. Baba atakuwa dhidi ya mwanawe, mwana dhidi ya baba yake; mama dhidi ya bintiye, binti dhidi ya mama yake; mamamkwe dhidi ya mke wa mwanawe na huyo dhidi ya mamamkwe wake.” Yesu akayaambia tena makundi ya watu, “Mnapoona mawingu yakitokea upande wa magharibi, mara mwasema: ‘Mvua itanyesha,’ na kweli hunyesha. Mnapoona upepo wa kusi unavuma, mwasema ‘Kutakuwa na joto,’ na ndivyo inavyokuwa. Enyi wanafiki! Mnajua kutabiri hali ya hewa kwa kuangalia hali ya nchi na anga; kwa nini, basi, hamwezi kujua maana ya nyakati hizi? “Na kwa nini hamwezi kujiamulia wenyewe jambo jema la kufanya? Maana kama mshtaki wako anakupeleka mahakamani, ingekuwa afadhali kwako kupatana naye mkiwa bado njiani, ili asije akakupeleka mbele ya hakimu, naye hakimu akakutoa kwa polisi, nao wakakutia ndani. Hakika hutatoka huko, nakuambia, mpaka utakapomaliza kulipa senti ya mwisho.” Wakati huo watu fulani walikuja, wakamweleza Yesu juu ya watu wa Galilaya ambao Pilato alikuwa amewaua wakati walipokuwa wanachinja wanyama wao wa tambiko. Naye Yesu akawaambia, “Mnadhani Wagalilaya hao walikuwa wahalifu kuliko Wagalilaya wengine, ati kwa sababu wameteseka hivyo? Nawaambieni hakika sivyo; lakini nanyi, hali kadhalika, msipotubu mtaangamia kama wao. Au wale kumi na wanane walioangukiwa na mnara kule Siloamu, wakafa; mnadhani wao walikuwa wakosefu kuliko wengine wote walioishi Yerusalemu? Nawaambieni sivyo; lakini nanyi msipotubu, mtaangamia kama wao.” Kisha, Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini shambani mwake. Mtu huyu akaenda akitaka kuchuma matunda yake, lakini akaukuta haujazaa hata tunda moja. Basi, akamwambia mfanyakazi wake: ‘Angalia! Kwa miaka mitatu nimekuwa nikija kuchuma matunda ya mtini huu, bila kupata chochote. Ukate! Kwa nini uitumie ardhi bure?’ Lakini yeye akamjibu: ‘Bwana, tuuache tena mwaka huu; nitauzungushia mtaro na kuutilia mbolea. Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vema; la sivyo, basi utaweza kuukata.’” Yesu alikuwa akifundisha katika sunagogi moja siku ya Sabato. Na hapo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na minane kutokana na pepo aliyekuwa amempagaa. Kwa sababu hiyo, mwili wake ulikuwa umepindika vibaya hata asiweze kusimama wima. Yesu alipomwona, alimwita, akamwambia, “Mama, umeponywa ugonjwa wako.” Akamwekea mikono, na mara mwili wake ukawa wima tena, akawa anamtukuza Mungu. Lakini mkuu wa sunagogi alikasirika kwa sababu Yesu alikuwa amemponya huyo mama siku ya Sabato. Hivyo akawaambia wale watu waliokusanyika pale, “Mnazo siku sita za kufanya kazi. Basi, fikeni siku hizo mkaponywe magonjwa yenu; lakini msije siku ya Sabato.” Hapo Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Nani kati yenu hangemfungua ng'ombe wake au punda wake kutoka zizini ampeleke kunywa maji, hata kama siku hiyo ni ya Sabato? Sasa, hapa yupo binti wa Abrahamu ambaye Shetani alimfanya kilema kwa muda wa miaka kumi na minane. Je, haikuwa vizuri kumfungulia vifungo vyake siku ya Sabato?” Alipokwisha sema hayo, wapinzani wake waliona aibu lakini watu wengine wote wakajaa furaha kwa sababu ya mambo yote aliyotenda. Yesu akauliza: “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaulinganisha na nini? Ni kama mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja na kuipanda shambani mwake; ikaota na kuwa mti. Ndege wa angani wakajenga viota vyao katika matawi yake.” Tena akauliza: “Nitaulinganisha ufalme wa Mungu na nini? Ni kama chachu aliyoitwaa mama mmoja na kuichanganya pamoja na unga madebe mawili na nusu kisha unga wote ukaumuka.” Yesu aliendelea na safari yake kwenda Yerusalemu huku akipitia mijini na vijijini, akihubiri. Mtu mmoja akamwuliza, “Je, Mwalimu, watu watakaookoka ni wachache?” Yesu akawaambia, “Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba; maana nawaambieni, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. Wakati utakuja ambapo mwenye nyumba atainuka na kufunga mlango. Nyinyi mtasimama nje na kuanza kubisha mlango mkisema: ‘Bwana, tufungulie mlango.’ Lakini yeye atawajibu: ‘Sijui mmetoka wapi.’ Nanyi mtaanza kumwambia: ‘Sisi ndio wale tuliokula na kunywa pamoja nawe; na wewe ulifundisha katika vijiji vyetu.’ Lakini yeye atasema: ‘Sijui nyinyi mmetoka wapi; ondokeni mbele yangu, enyi nyote watenda maovu.’ Ndipo kutakuwa na kulia na kusaga meno, wakati mtakapowaona Abrahamu, Isaka na Yakobo na manabii wote wapo katika ufalme wa Mungu, lakini nyinyi wenyewe mmetupwa nje! Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini na kukaa kwenye karamu katika ufalme wa Mungu. Naam, wale walio wa mwisho watakuwa wa kwanza; na wale walio wa kwanza watakuwa wa mwisho.” Wakati huohuo, Mafarisayo na watu wengine walimwendea Yesu wakamwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine, kwa maana Herode anataka kukuua.” Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie huyo mbweha hivi: ‘Leo na kesho ninafukuza pepo na kuponya wagonjwa, na siku ya tatu nitakamilisha kazi yangu.’ Hata hivyo, kwa leo, kesho na kesho kutwa, ni lazima niendelee na safari yangu, kwa sababu si sawa nabii auawe nje ya Yerusalemu. “Yerusalemu! Ee Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako. Mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako pamoja kama kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka. Haya! Utaachiwa mwenyewe nyumba yako. Basi, nawaambieni, hamtaniona mpaka wakati utakapofika mseme: ‘Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.’” Siku moja ya Sabato, Yesu alikwenda kula chakula nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo, na watu waliokuwapo hapo wakawa wanamchunguza. Mbele yake Yesu palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na ugonjwa wa kuvimba mwili. Yesu akawauliza waalimu wa sheria na Mafarisayo, “Je, ni halali au la kumponya mtu siku ya Sabato?” Lakini wao wakakaa kimya. Yesu akamshika huyo mgonjwa, akamponya, akamwacha aende zake. Halafu akawaambia, “Ni nani kati yenu ambaye mtoto wake au ng'ombe wake akitumbukia shimoni, hangemtoa hata kama ni siku ya Sabato?” Nao hawakuweza kumjibu swali hilo. Yesu aliona jinsi wale walioalikwa walivyokuwa wanajichagulia nafasi za heshima, akawaambia mfano: “Kama mtu akikualika harusini, usiketi mahali pa heshima, isije ikawa amealikwa mwingine mheshimiwa kuliko wewe; na mwenyeji wenu nyinyi wawili atakuja na kukuambia: ‘Mwachie huyu nafasi.’ Hapo utaaibika mbele ya wote na kulazimika kwenda kuchukua nafasi ya mwisho. Bali ukialikwa kwenye karamu, keti mahali pa mwisho, ili mwenyeji wako atakapokuja akuambie: ‘Rafiki, njoo hapa mbele, mahali pazuri zaidi.’ Hapo utakuwa umeheshimika mbele ya wote wanaoketi pamoja nawe. Kwa maana yeyote anayejikweza atashushwa na anayejishusha, atakwezwa.” Halafu akamwambia na yule aliyemwalika, “Kama ukiwaandalia watu karamu mchana au jioni, usiwaalike rafiki zako au jamaa zako au jirani zako walio matajiri wasije nao wakakualika, nawe ukawa umelipwa kile ulichowatendea. Badala yake, unapofanya karamu, waalike maskini, vilema, viwete na vipofu, nawe utakuwa umepata baraka, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa. Maana Mungu atakupa tuzo lako wakati watu wema watakapofufuka.” Mmoja wa wale waliokuwa wameketi pamoja na Yesu akasema, “Ana heri mtu yule atakayekula chakula katika ufalme wa Mungu.” Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akawaalika watu wengi. Wakati wa karamu ulipofika alimtuma mtumishi wake akawaambie walioalikwa, ‘Njoni, kila kitu ni tayari.’ Lakini wote, mmoja baada ya mwingine, wakaanza kuomba radhi. Wa kwanza akamwambia mtumishi: ‘Nimenunua shamba, na hivyo sina budi niende kuliangalia; nakuomba uniwie radhi.’ Mwingine akasema: ‘Nimenunua ng'ombe jozi tano wa kulima, sasa nimo njiani kwenda kuwajaribu; nakuomba uniwie radhi.’ Na mwingine akasema: ‘Nimeoa kwa hiyo siwezi kuja.’ Mtumishi huyo akarudi na kumwarifu bwana wake jambo hilo. Yule mwenye nyumba alikasirika, akamwambia mtumishi wake: ‘Nenda upesi kwenye barabara na vichochoro vya mji, uwalete hapa ndani maskini, viwete, vipofu na vilema wengine.’ Baadaye, mtumishi huyo akasema: ‘Bwana, mambo yamefanyika kama ulivyoamuru, lakini bado iko nafasi.’ Yule bwana akamwambia mtumishi: ‘Nenda katika barabara na vichochoro vya mji uwashurutishe watu kuingia ili nyumba yangu ijae. Kwa maana, nawaambieni, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeonja karamu yangu.’” Hapo, makundi mengi yakawa yanaandamana pamoja na Yesu. Basi, akawageukia watu akawaambia, “Mtu yeyote akija kwangu, asipomchukia baba yake, mama yake, mke wake, watoto, ndugu na dada zake, naam, hata na nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Kwa maana, ni nani miongoni mwenu ambaye akitaka kujenga mnara hataketi kwanza akadirie gharama zake ili ajue kama ana kiasi cha kutosha cha kumalizia? La sivyo, baada ya kuweka msingi na kushindwa kumaliza, watu watamcheka wakisema: ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini hakumalizia.’ “Au, ni mfalme gani ambaye akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, hataketi kwanza na kufikiri kama ataweza, kwa askari wake10,000, kumkabili yule aliye na askari 20,000? Kama anaona hataweza, atawatuma wajumbe kutaka masharti ya amani wakati mfalme huyo mwingine angali mbali. Vivyo hivyo, basi, hakuna hata mmoja wenu atakayekuwa mwanafunzi wangu kama asipoachilia kila kitu alicho nacho. “Chumvi ni nzuri; lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini? Haifai kitu wala kwa udongo wala kwa mbolea. Watu huitupilia mbali. Mwenye masikio na asikie!” Siku moja, watozaushuru na wenye dhambi wengi walikwenda kumsikiliza Yesu. Mafarisayo na waalimu wa sheria wakaanza kunungunika: “Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao.” Yesu akawajibu kwa mfano: “Hivi, mmoja wenu akiwa na kondoo 100, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate. Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha. Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.’ Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu. “Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, ataifagia nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate. Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake na kusema, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.’ Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu.” Yesu akaendelea kusema, “Kulikuwa na mtu mmoja mwenye watoto wawili wa kiume. Yule mdogo alimwambia baba yake: ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Naye akawagawia mali yake. Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo. Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika. Akaomba kazi kwa mwananchi mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe. Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu. Alipoanza kupata akili, akafikiri: ‘Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa? Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu. “Mwanae akamwambia: ‘Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.’ Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: ‘Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu! Mchinjeni ndama mnono; tule na kusherehekea! Kwa sababu huyu mwanangu; alikuwa amekufa, kumbe yu hai; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kufanya sherehe. “Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani, akasikia vifijo na ngoma. Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: ‘Kuna nini?’ Huyo mtumishi akamwambia: ‘Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.’ Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie. Lakini yeye akamjibu: ‘Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwanambuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu! Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.’ Baba yake akamjibu: ‘Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako. Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’” Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Tajiri mmoja alikuwa na karani wake. Huyu karani alichongewa kwamba alitumia ovyo mali ya tajiri wake. Yule tajiri akamwita, akamwambia: ‘Ni mambo gani haya ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya mapato na matumizi ya mali yangu, kwa maana huwezi kuwa karani tena.’ Yule karani akafikiri: ‘Bwana wangu amenifukuza kazi ya ukarani; nitafanya nini? Kwenda kulima siwezi; kwenda kuombaomba kama maskini ni aibu. Naam, najua la kufanya, ili nitakapofukuzwa kazi, watu waweze kunikaribisha nyumbani kwao.’ Basi, akawaita wadeni wa bwana wake, mmojammoja, akamwambia yule wa kwanza: ‘Unadaiwa kiasi gani na bwana wangu?’ Yeye akamjibu: ‘Mapipa 100 ya mafuta ya zeituni.’ Yule karani akamwambia: ‘Chukua hati yako ya deni, keti haraka, andika hamsini.’ Kisha akamwuliza mdeni mwingine: ‘Wewe unadaiwa kiasi gani?’ Yeye akamjibu: ‘Magunia 100 ya ngano.’ Yule karani akamwambia: ‘Chukua hati yako ya deni, andika themanini.’ “Basi, yule bwana akamsifu huyo karani asiye mwaminifu, kwa kuwa alitumia busara. Kwa maana watu wa dunia hii wana busara zaidi na mambo yao kuliko watu wa mwanga.” Naye Yesu akaendelea kusema, “Nami nawaambieni, jifanyieni marafiki kutokana na mali ya dunia, ili zitakapowaishieni, wawapokeeni katika makao ya milele. Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, atakuwa mwaminifu katika mambo makubwa; na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo, hatakuwa mwaminifu katika mambo makubwa. Kama basi, nyinyi si waaminifu kuhusu mali mbaya za dunia, ni nani atakayewakabidhi zile mali za kweli? Na kama nyinyi si waaminifu kuhusu mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewakabidhi mali yenu wenyewe? “Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au ataambatana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali pamoja.” Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, kwa vile wao walikuwa wanapenda sana fedha, wakamdharau Yesu. Hapo akawaambia, “Nyinyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka. “Sheria na maandishi ya manabii vilikuwako mpaka wakati wa Yohane Mbatizaji. Tangu hapo, ufalme wa Mungu unahubiriwa, na kila mmoja anauingia kwa nguvu. Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita, kuliko hata herufi moja ya sheria kufutwa. “Yeyote anayempa mkewe talaka na kuoa mwingine, anazini; na yeyote anayemwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini. “Palikuwa na mtu mmoja tajiri, ambaye alikuwa anavaa mavazi ya bei kubwa sana ya rangi ya zambarau na ya kitani safi, na kufanya sherehe kila siku. Na, mlangoni pa huyo tajiri kulikuwa na maskini mmoja jina lake Lazaro, ambaye alikuwa amejaa vidonda. Lazaro alitamani kupewa makombo yaliyoanguka kutoka mezani pa huyo tajiri; na zaidi ya hayo, mbwa walikuwa wanakuja na kuramba vidonda vyake! “Basi, huyo maskini akafa, nao malaika wakamchukua, wakamweka karibu na Abrahamu. Na yule tajiri pia akafa, akazikwa. Huyo tajiri, akiwa na mateso makali huko kuzimu, akainua macho yake, akamwona Abrahamu kwa mbali na Lazaro karibu naye. Basi, akaita kwa sauti: ‘Babu Abrahamu, nionee huruma; umtume Lazaro angalau achovye ncha ya kidole chake katika maji, auburudishe ulimi wangu, maana ninateseka mno katika moto huu.’ Lakini Abrahamu akamjibu: ‘Kumbuka mwanangu kwamba ulipokea mema yako katika maisha, naye Lazaro akapokea mabaya. Sasa lakini, yeye anatulizwa, nawe unateswa. Licha ya hayo, kati yetu na nyinyi kumewekwa shimo kubwa, ili wanaotaka kuja kwenu kutoka huku wasiweze, na wanaotaka kutoka kwenu kuja kwetu wasiweze.’ Huyo aliyekuwa tajiri akasema: ‘Basi babu, nakuomba umtume aende nyumbani kwa baba yangu, maana ninao ndugu watano, ili awaonye wasije wakaja huku kwenye mateso.’ Lakini Abrahamu akamwambia: ‘Ndugu zako wanao Mose na manabii; waache wawasikilize hao.’ Lakini yeye akasema: ‘Sivyo babu Abrahamu, ila kama mtu atafufuka kutoka kwa wafu na kuwaendea, watatubu.’ Naye Abrahamu akasema: ‘Kama hawawasikilizi Mose na manabii, hawatajali hata kama mtu angefufuka kutoka kwa wafu.’” Kisha, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Haiwezekani kabisa kusitokee vikwazo vinavyosababisha dhambi; lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha. Ingekuwa afadhali kwake kufungiwa shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini, kuliko kumkwaza mmoja wa wadogo hawa. Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, muonye; akitubu, msamehe. Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema, ‘Nimetubu,’ lazima umsamehe.” Mitume wakamwambia Bwana, “Utuongezee imani.” Naye Bwana akajibu, “Kama imani yenu ingekuwa ndogo hata kama chembe ndogo ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu: ‘Ngoka ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii. “Tuseme mmoja wenu ana mtumishi ambaye analima shambani au anachunga kondoo. Je, anaporudi kutoka shambani, atamwambia huyo mtumishi: ‘Haraka, njoo ule chakula?’ La! Atamwambia: ‘Nitayarishie chakula, ujifunge tayari kunitumikia mpaka nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo nawe ule na kunywa.’ Je, utamshukuru huyo mtumishi kwa sababu ametimiza aliyoamriwa? Hali kadhalika na nyinyi mkisha fanya yote mliyoamriwa, semeni: ‘Sisi ni watumishi tusio na faida, tumetimiza tu yale tuliyotakiwa kufanya.’” Yesu akiwa safarini kwenda Yerusalemu alipitia katika mipaka ya Samaria na Galilaya. Alipokuwa anaingia katika kijiji kimoja, watu kumi wenye ukoma walikutana naye, wakasimama kwa mbali. Wakapaza sauti wakisema, “Yesu Mwalimu, tuonee huruma!” Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.” Basi, ikawa walipokuwa wanakwenda, wakatakasika. Mmoja wao alipoona kwamba ameponywa, alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa. Akajitupa chini mbele ya miguu ya Yesu huku akimshukuru. Huyo alikuwa Msamaria. Hapo Yesu akasema, “Je, si watu kumi walitakaswa? Wale tisa wako wapi? Hakupatikana mwingine aliyerudi kumtukuza Mungu ila tu huyu mgeni?” Halafu akamwambia huyo mtu, “Simama, uende zako; imani yako imekuponya.” Wakati mmoja, Mafarisayo walimwuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Naye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa namna itakayoweza kuonekana. Wala hakuna atakayeweza kusema, ‘Uko hapa’, au ‘Uko pale’. Kwa kweli ufalme wa Mungu uko kati yenu.” Halafu akawaambia wanafunzi wake, “Siku zinakuja ambapo mtatamani kuona mojawapo ya siku za Mwana wa Mtu, lakini hamtaiona. Na watu watawaambieni: ‘Tazameni, yuko pale!’ Au ‘Tazameni, yupo hapa!’ Lakini nyinyi msitoke wala msiwafuate. Kwa maana kama vile umeme unavyotokea ghafla na kuangaza anga upande mmoja hadi mwingine, ndivyo Mwana wa Mtu atakavyokuwa siku ile yake. Lakini kabla ya hayo, itambidi ateseke sana na kukataliwa na kizazi hiki. Kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Mtu. Watu waliendelea kula na kunywa, kuoa na kuolewa mpaka wakati ule Noa alipoingia katika safina. Gharika ikatokea na kuwaangamiza wote. Itakuwa kama ilivyotokea wakati wa Loti. Watu waliendelea kula na kunywa, kununua na kuuza, kupanda mbegu na kujenga. Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, moto na madini ya kiberiti vikanyesha kama mvua kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote. Ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Mtu atakapofunuliwa. “Siku hiyo, yeyote atakayekuwa juu ya paa asishuke kwenda nyumbani kuchukua mali yake. Kadhalika, naye atakayekuwa shambani asirudi nyuma. Kumbukeni yaliyompata mke wa Loti. Yeyote anayetaka kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na yeyote anayeipoteza, ataiokoa. Nawaambieni, siku ile usiku watu wawili watakuwa wanalala pamoja, mmoja atachukuliwa na yule mwingine ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga nafaka pamoja; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.” [ Watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.] Hapo wakamwuliza, “Ni wapi Bwana?” Naye akawaambia, “Palipo mzoga, ndipo tai watakapokusanyikia.” Basi, Yesu aliwasimulia mfano kuonesha kwamba ni lazima kusali daima bila kukata tamaa. Alisema: “Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu ambaye hakuwa anamcha Mungu wala kumjali binadamu. Katika mji huohuo, kulikuwa pia na mama mmoja mjane ambaye alimwendea huyo hakimu mara nyingi akimwomba amtetee apate haki yake kutoka kwa adui yake. Kwa muda mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea: ‘Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu, lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa, na mwisho atanichosha kabisa!’” Basi, Bwana akaendelea kusema, “Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya. Je, ndio kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasikiliza? Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?” Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine. “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali: Mmoja Mfarisayo, na mwingine mtozaushuru. Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: ‘Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: Walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtozaushuru. Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.’ Lakini yule mtozaushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: ‘Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.’ Nawaambieni, huyu mtozaushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa.” Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali. Lakini Yesu akawaita kwake akisema: “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa. Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika ufalme huo.” Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuupata uhai wa milele?” Yesu akamwambia, “Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake. Unazijua amri: ‘Usizini; Usiue; Usiibe; Usitoe ushahidi wa uongo; Waheshimu baba yako na mama yako.’” Yeye akasema, “Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu.” Yesu aliposikia hayo, akamwambia, “Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: Uza kila kitu ulicho nacho, wagawie maskini hiyo fedha, nawe utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate.” Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana. Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, “Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu! Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Wale watu waliposikia hayo, wakasema, “Nani basi, atakayeokolewa?” Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu.” Naye Petro akamwuliza, “Na sisi, je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!” Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au ndugu au wazazi au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu, atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na uhai wa milele wakati ujao.” Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa. Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate. Watampiga mijeledi na kumuua; lakini siku ya tatu atafufuka.” Lakini wao hawakuelewa jambo hilo hata kidogo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa. Wakati Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba. Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, “Kuna nini?” Wakamwambia, “Yesu wa Nazareti anapita.” Naye akapaza sauti akisema, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!” Wale watu waliotangulia wakamkemea wakimwambia anyamaze; lakini yeye akazidi kupaza sauti: “Mwana wa Daudi, nihurumie!” Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake. Yule kipofu alipofika karibu, Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Naye akamjibu, “Bwana, naomba nipate kuona.” Yesu akamwambia, “Ona! Imani yako imekuponya.” Na mara huyo kipofu akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu. Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa akipita katika njia za mji huo. Palikuwa na mtu mmoja huko mjini aitwaye Zakayo ambaye alikuwa mkuu wa watozaushuru, na pia mtu tajiri. Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu. Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu ili aweze kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo. Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, “Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako.” Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha. Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunungunika wakisema, “Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi.” Lakini Zakayo akasimama, akamwambia Yesu, “Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyanganya mtu yeyote kitu, nitamrudishia mara nne.” Yesu akamwambia, “Leo wokovu umefika katika nyumba hii, kwa vile huyu pia ni wa ukoo wa Abrahamu. Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea.” Wakati watu walipokuwa bado wanasikiliza hayo, Yesu akawaambia mfano. Hapo alikuwa anakaribia Yerusalemu, na watu wale walidhani kwamba muda si muda, ufalme wa Mungu ungefika. Hivyo akawaambia, “Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme, halafu arudi. Basi, kabla ya kuondoka, aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kuwaambia: ‘Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.’ Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende wakaseme: ‘Hatumtaki huyu atutawale.’ “Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili aweze kujua kila mmoja amepata faida gani. Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: ‘Bwana, faida iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.’ Naye akamwambia: ‘Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!’ Mtumishi wa pili akaja, akasema: ‘Bwana, faida iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.’ Naye akamwambia pia: ‘Nawe utakuwa na madaraka juu ya miji mitano.’ “Mtumishi mwingine akaja, akasema: ‘Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa, kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na kuchuma ambacho hukupanda.’ Naye akamwambia: ‘Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda. Kwa nini, basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?’ Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: ‘Mnyanganyeni hiyo fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.’ Nao wakamwambia: ‘Lakini Bwana, huyo ana faida ya kiasi hicho mara kumi!’ Naye akawajibu: ‘Kila aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. Na sasa, kuhusu hao maadui zangu ambao hawapendi niwe mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu.’” Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu. Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia: “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwanapunda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungueni, mkamlete hapa. Kama mtu akiwauliza kwa nini mnamfungua, mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’” Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia. Walipokuwa wanamfungua yule mwanapunda, wenyewe wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua mwanapunda huyu?” Nao wakawajibu, “Bwana anamhitaji.” Basi, wakampelekea Yesu yule mwanapunda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake, wakampandisha Yesu juu yake. Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani. Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona; wakawa wanasema: “Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!” Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu wakamwambia Yesu, “Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!” Yesu akawajibu, “Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti.” Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia akisema: “Laiti ungelijua leo hii mambo yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako. Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote. Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa.” Kisha, Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwafukuza nje wafanyabiashara akisema, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala’; lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi.” Yesu akawa anafundisha kila siku hekaluni. Makuhani wakuu, waalimu wa sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza, lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini kabisa. Siku moja, Yesu alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni na kuwahubiria juu ya Habari Njema, makuhani wakuu na waalimu wa sheria pamoja na wazee walifika, wakasema, “Tuambie! Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani?” Yesu akawaambia, “Na mimi nitawaulizeni swali: Mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa Mungu au kwa watu?” Lakini wao wakajadiliana hivi: “Tukisema yalitoka kwa Mungu, yeye atatuuliza: ‘Mbona hamkumsadiki?’ Na tukisema yalitoka kwa binadamu, watu wote hapa watatupiga mawe, maana wote wanaamini kwamba Yohane alikuwa nabii.” Basi, wakamwambia, “Hatujui mamlaka hayo yalitoka wapi.” Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.” Yesu akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima; kisha akasafiri hadi nchi ya mbali, akakaa huko kwa muda mrefu. Wakati wa mavuno, mtu huyo alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima, akachukue sehemu ya matunda ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga mtumishi huyo, wakamrudisha mikono mitupu. Yule bwana akamtuma tena mtumishi mwingine; lakini wao wakampiga huyo vilevile na kumtendea vibaya, wakamrudisha mikono mitupu. Akamtuma tena wa tatu; huyu naye, baada ya kumwumiza, wakamfukuza. Yule mwenye shamba akafikiri: ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpenzi; labda watamjali yeye.’ Wale wakulima walipomwona tu, wakasemezana: ‘Huyu ndiye mrithi. Basi, tumuue ili urithi wake uwe wetu.’ Basi, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua.” Yesu akauliza, “Yule mwenye shamba atawafanya nini hao wakulima? Atakuja kuwaangamiza wakulima hao, na kuwapa wakulima wengine hilo shamba la mizabibu.” Watu waliposikia maneno hayo, walisema: “Hasha! Yasitukie hata kidogo!” Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Maandiko haya Matakatifu yana maana gani, basi? ‘Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi!’ Mtu yeyote akianguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda.” Waalimu wa sheria na makuhani wakuu walifahamu kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu, na hivyo walitaka kumkamata palepale, ila tu waliogopa watu. Basi, wakawa wanatafuta wakati wa kufaa. Wakawahonga watu fulani wajisingizie kuwa wema, wakawatuma wamnase Yesu kwa maswali, na hivyo waweze kumtia nguvuni na kumpeleka kwa wakuu wa serikali. Hao wapelelezi wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba unasema na kufundisha mambo ya kweli; tunajua kwamba wewe huna ubaguzi; wewe wafundisha ukweli juu ya njia ya Mungu. Basi, tuambie kama ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari!” Yesu alitambua mtego wao, akawaambia, “Nionesheni sarafu. Je, sura na chapa ni vya nani?” Nao wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” Hawakufaulu kumnasa kwa neno lolote pale mbele ya watu na hivyo wakakaa kimya wakilistaajabia jibu lake. Kisha Masadukayo, ambao husema kwamba wafu hawafufuki, wakamjia Yesu, wakasema: “Mwalimu, Mose alituandikia kwamba kama ndugu ya mtu fulani akifa na kumwacha mjane wake bila watoto, ni lazima ndugu yake amchukue huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto. Sasa, wakati mmoja kulikuwa na ndugu saba. Yule wa kwanza alioa na baadaye akafa bila kuacha mtoto. Yule ndugu wa pili akamwoa yule mjane, naye pia akafa; na ndugu wa tatu vilevile. Mambo yakawa yaleyale kwa wote saba — wote walikufa bila kuacha watoto. Mwishowe akafa pia yule mwanamke. Je, siku wafu watakapofufuliwa, mama huyo atakuwa mke wa nani? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.” Yesu akawaambia, “Watu wa nyakati hizi huoa na kuolewa; lakini wale ambao Mungu atawawezesha kushiriki ule wakati wa ufufuo, hawataoa wala kuolewa. Ama hakika, hawawezi kufa tena, kwa sababu watakuwa kama malaika, na ni watoto wa Mungu kwa vile wamefufuliwa katika wafu. Lakini, kwamba kuna kufufuka kutoka kwa wafu, hata Mose alithibitisha jambo hilo katika Maandiko Matakatifu. Katika sehemu ya Maandiko Matakatifu juu ya kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto, anamtaja Bwana kama Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa wale walio hai; maana kwake wote wanaishi.” Baadhi ya wale waalimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, umejibu vema kabisa.” Walisema hivyo kwa sababu hawakuthubutu kumwuliza tena maswali mengine. Yesu akawauliza, “Yasemekanaje kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? Daudi mwenyewe anasema katika Zaburi: ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia mpaka niwaweke maadui zako kuwa kiti cha kuwekea miguu yako.’ Ikiwa Daudi anamwita yeye, ‘Bwana,’ basi, atakuwaje mwanawe?” Yesu aliwaambia wanafunzi wake mbele ya watu wote, “Jihadharini na waalimu wa sheria ambao hupenda kupitapita wamevalia kanzu. Hupenda kusalimiwa na watu kwa heshima masokoni, huketi mahali pa heshima katika masunagogi na kuchukua nafasi za heshima katika karamu. Huwadhulumu wajane huku wakisingizia kuwa wema kwa kusali sala ndefu. Hao watapata hukumu kali zaidi!” Yesu alitazama kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya hekalu, akamwona pia mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo. Basi, akasema, “Nawaambieni kweli, mama huyu mjane maskini ametia katika hazina kiasi kikubwa kuliko walichotia wote. Kwa maana, wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi.” Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema, “Haya yote mnayoyaona — zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa.” Basi, wakamwuliza, “Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani zitakazoonesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?” Yesu akawajibu, “Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu, kila mmoja akidai kwamba yeye ni mimi, na kwamba wakati ule umekaribia. Lakini nyinyi msiwafuate! Basi, mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado.” Halafu akaendelea kusema: “Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani. Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu, mpate kunishuhudia kwao. Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: Hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea, kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hata maadui zenu hawataweza kustahimili wala kupinga. Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti nyinyi; na baadhi yenu mtauawa. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea. Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu. “Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi jueni ya kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa. Hapo, walioko Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani wasirudi mjini. Kwa maana siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie. Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa. Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia. “Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari. Watu watazirai kwa sababu ya woga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa. Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi. Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia.” Kisha akawaambia mfano: “Angalieni mtini na miti mingine yote. Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba majira ya mavuno yamekaribia. Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka, mtatambua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia. Kweli nawaambieni, kizazi hiki cha sasa hakitapita kabla ya hayo yote kutendeka. Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. “Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, siku ile itawajieni ghafla. Kwa maana itawajia kama mtego wote wanaoishi duniani pote. Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu.” Wakati wa mchana, siku hizo, Yesu alikuwa akifundisha watu hekaluni; lakini usiku alikuwa akienda katika mlima wa Mizeituni na kukaa huko. Watu wote walikuwa wanakwenda hekaluni asubuhi na mapema, wapate kumsikiliza. Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa inakaribia. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria wakawa wanatafuta njia ya kumwua Yesu, lakini waliwaogopa watu. Basi, Shetani akamwingia Yuda aitwaye Iskarioti, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda, akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao. Nao wakafurahi na kupatana naye kumlipa fedha. Yuda akakubali, na akawa anatafuta nafasi nzuri ya kumkabidhi kwao bila umati wa watu kujua. Basi, siku ya mikate isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa. Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, “Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka.” Nao wakamwuliza, “Unataka tuiandae wapi?” Akawaambia, “Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia. Mwambieni mwenye nyumba: ‘Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ Naye atawaonesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo.” Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka. Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake. Akawaambia, “Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. Maana nawaambieni, sitaila tena hadi hapo itakapokamilika katika ufalme wa Mungu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akasema, “Pokeeni, mgawane. Kwa maana nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka ufalme wa Mungu utakapokuja.” Halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka.” Akafanya vivyo hivyo na kikombe cha divai baada ya chakula, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu inayomwagika kwa ajili yenu. “Lakini, tazameni! Yule atakayenisaliti yuko nami hapa mezani. Kweli Mwana wa Mtu anakwenda kuuawa kama ilivyopangwa, lakini ole wake mtu anayemsaliti.” Hapo wakaanza kuulizana wao kwa wao ni nani kati yao atakayefanya jambo hilo. Kulitokea ubishi kati ya hao mitume kuhusu nani miongoni mwao anayefikiriwa kuwa mkuu kuliko wengine. Yesu akawaambia, “Wafalme wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, nao huitwa wafadhili wa watu. Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi. Kwa maana, ni nani aliye mkuu: Yule anayeketi mezani kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi. “Nyinyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu yangu; na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi ufalme, vivyo hivyo nami ninawakabidhi nyinyi ufalme. Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu na kuketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. “Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka kuwapepeta nyinyi kama mtu anavyopepeta ngano. Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako.” Naye Petro akamjibu, “Bwana, mimi niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani, na hata kufa.” Yesu akamjibu, “Nakuambia wewe Petro, kabla jogoo hajawika leo utakuwa umenikana mara tatu.” Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, “Wakati nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa chochote?” Wakajibu, “La.” Naye akawaambia, “Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja. Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: ‘Aliwekwa kundi moja na wahalifu,’ ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake.” Nao wakasema, “Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili.” Naye akasema, “Basi!” Yesu akatoka, na kama ilivyokuwa desturi yake, akaenda katika mlima wa Mizeituni; wanafunzi wake wakamfuata. Alipofika huko akawaambia, “Salini, msije mkaingia katika kishawishi.” Kisha akawaacha, akaenda umbali wa mtu kuweza kutupa jiwe, akapiga magoti, akasali: “Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki; hata hivyo, mapenzi yako yatimizwe, wala siyo yangu.” Hapo, malaika kutoka mbinguni akamtokea ili kumtia moyo. Akiwa katika uchungu mkubwa, alisali kwa bidii zaidi; na jasho likamtoka kama matone ya damu, likatiririka mpaka chini. Baada ya kusali, aliwarudia wanafunzi wake, akawakuta wamelala, kwani walikuwa na huzuni. Akawaambia, “Mbona mnalala? Amkeni msali, msije mkaingia katika kishawishi.” Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa kumbusu. Lakini Yesu akamwambia, “Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?” Wale wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, “Bwana, tutumie panga zetu?” Na mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio lake la kulia. Hapo, Yesu akasema, “Acha! Hii inatosha.” Akaligusa sikio la mtu huyo, akaliponya. Kisha Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa hekalu na wazee waliokuja kumkamata: “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza.” Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa kuhani mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali. Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja, naye Petro akiwa miongoni mwao. Mtumishi mmoja wa kike alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, “Mtu huyu pia alikuwa pamoja na Yesu.” Lakini Petro akakana akisema, “Wee! Simjui mimi.” Baadaye kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, “Wewe ni mmoja wao.” Lakini Petro akajibu “Bwana wee; si mimi!” Kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, “Hakika huyu alikuwa pamoja naye; ametoka Galilaya ati.” Lakini Petro akasema, “Bwana wee; sijui hata unachosema!” Na papo hapo, akiwa bado anaongea, jogoo akawika. Bwana akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: “Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Hapo akatoka nje, akalia sana. Wale watu waliokuwa wanamchunga Yesu, walimpiga na kumdhihaki. Walimfunga kitambaa usoni, wakawa wanamwuliza, “Ni nani aliyekupiga? Hebu bashiri, tuone!” Wakamtolea maneno mengi ya matusi. Kulipokucha, kikao cha wazee wa watu kilifanyika, ambacho kilihudhuriwa na makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Yesu akaletwa mbele ya Baraza hilo. Nao wakamwambia, “Tuambie! Je, wewe ndiwe Kristo?” Lakini Yesu akawaambia, “Hata kama nikiwaambieni, hamtasadiki; na hata kama nikiwaulizeni swali, hamtanijibu. Lakini tangu sasa, Mwana wa Mtu atakuwa ameketi upande wa kulia wa Mungu Mwenye Nguvu.” Hapo wote wakasema, “Ndiyo kusema wewe ni Mwana wa Mungu?” Naye akasema, “Nyinyi mnasema kwamba mimi ndiye.” Nao wakasema, “Je, tunahitaji ushahidi mwingine? Sisi wenyewe tumesikia akisema kwa mdomo wake mwenyewe.” Kisha, wote kwa jumla, wakasimama, wakampeleka Yesu mbele ya Pilato. Wakaanza kumshtaki wakisema: “Tulimkuta mtu huyu akiwapotosha watu wetu, akipinga kulipa kodi kwa Kaisari na kujiita ati yeye ni Kristo, Mfalme.” Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamjibu, “Wewe umesema.” Pilato akawaambia makuhani wakuu na umati wa watu, “Sioni kosa lolote katika mtu huyu.” Lakini wao wakasisitiza wakisema: “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika nchi yote ya Yudea; alianza Galilaya, na sasa yuko hapa.” Pilato aliposikia hayo, akauliza, “Je, mtu huyu ni mwenyeji wa Galilaya?” Alipojua kwamba Yesu alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa Yerusalemu. Herode alifurahi sana alipomwona Yesu. Alikuwa amekwisha sikia habari zake, na hivyo alikuwa anatazamia kwa muda mrefu kumwona kwa macho yake mwenyewe. Zaidi ya hayo, alikuwa anatumaini kumwona Yesu akitenda mwujiza. Basi, akamwuliza maswali mengi kwa muda mrefu, lakini Yesu hakumjibu neno. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria wakajitokeza mbele, wakatoa mashtaka yao kwa nguvu sana. Basi, Herode pamoja na askari wake, wakamwaibisha Yesu na kumfanyia mzaha; kisha wakamvika vazi la kifalme, wakamrudisha kwa Pilato. Herode na Pilato, ambao hapo awali walikuwa maadui, tangu siku hiyo wakawa marafiki. Basi, Pilato akaitisha mkutano wa makuhani wakuu, viongozi na watu, akawaambia, “Mmemleta mtu huyu kwangu mkisema kwamba alikuwa anawapotosha watu. Sasa sikilizeni! Baada ya kuchunguza jambo hilo mbele yenu, sikumpata na kosa lolote kuhusu mashtaka yenu juu yake. Wala si mimi tu, bali hata Herode hakuona kosa lolote, kwa maana amemrudisha kwangu. Ni dhahiri kwamba mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo. Hivyo, nitaamuru apigwe viboko, halafu nitamwachilia.” [ Kila sikukuu ya Pasaka, ilimlazimu Pilato kuwafungulia mfungwa mmoja.] Lakini wote wakapiga kelele pamoja: “Mwondoe huyo, utufungulie Baraba!” ( Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika mji na pia kwa sababu ya kuua.) Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena; lakini wao wakapiga kelele: “Msulubishe, msulubishe!” Pilato akawaambia mara ya tatu, “Amefanya ubaya gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko, halafu nimwachilie.” Lakini wao wakazidi kupiga kelele kwa nguvu sana, kwamba Yesu ni lazima asulubiwe. Mwishowe, sauti zao zikashinda. Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe. Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye alikuwa ametiwa gerezani kwa kusababisha uasi na mauaji; akamtoa Yesu kwao, wamfanyie walivyotaka. Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule msalaba auchukue nyuma ya Yesu. Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia. Yesu akawageukia, akasema, “Enyi kina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu. Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: ‘Heri yao wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!’ Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima: ‘Tuangukieni!’ Na vilima, ‘Tufunikeni!’ Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?” Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe pamoja naye. Walipofika mahali paitwapo, “Fuvu la Kichwa,” ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. Yesu akasema, “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya.” Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: “Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!” Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki wakisema: “Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.” Vilevile maandishi haya yalikuwa yamewekwa juu yake: “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.” Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: “Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia.” Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: “Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo. Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.” Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.” Yesu akamjibu, “Nakuambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.” Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likaifunika nchi yote mpaka saa tisa, na pazia lililokuwa limetundikwa hekaluni likapasuka vipande viwili. Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho. Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: “Hakika huyu alikuwa mtu mwema.” Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni. Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo. Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Arimathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika. Alikuwa akitazamia kuja kwa ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza Kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao. Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Kisha akaushusha mwili huo kutoka msalabani, akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika. Siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na maandalio ya siku ya Sabato yalikuwa yanaanza. Wale wanawake walioandamana na Yesu kutoka Galilaya walimfuata Yosefu, wakaliona lile kaburi na jinsi mwili wake Yesu ulivyowekwa. Halafu, walirudi nyumbani, wakatayarisha manukato na marashi ya kuupaka mwili wa Yesu. Siku ya Sabato walipumzika kama ilivyoamriwa na sheria. Jumapili, alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda kaburini wakichukua yale manukato waliyotayarisha. Walikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi. Walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. Walipokuwa bado wanashangaa juu ya jambo hilo, mara watu wawili waliovaa mavazi yenye kungaa sana, wakasimama karibu nao. Hao wanawake wakaingiwa na hofu, wakainama chini. Ndipo wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu? Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni alipokuwa kule Galilaya: ‘Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao watamsulubisha na siku ya tatu atafufuka.’” Hapo hao wanawake wakayakumbuka maneno yake, wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wafuasi wengine habari za mambo hayo yote. Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao. Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini. Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini. Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa anashangaa juu ya hayo yaliyotokea. Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu. Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia. Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao. Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua. Akawauliza, “Mnazungumza nini huku mnatembea?” Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni. Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, “Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?” Naye akawajibu, “Mambo gani?” Wao wakamjibu, “Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote. Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha. Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka. Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi, wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai. Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona.” Kisha Yesu akawaambia, “Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii? Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?” Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote. Walipokikaribia kile kijiji walichokuwa wanakiendea, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari; lakini wao wakamsihi wakisema, “Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia.” Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao. Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao. Basi, wakaambiana, “Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?” Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu; wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao wamekusanyika wakisema, “Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni.” Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate. Walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia “Amani iwe nanyi.” Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu. Lakini yeye akawaambia, “Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu? Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkaone, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo.” Baada ya kusema hayo, akawaonesha mikono na miguu. Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, “Mnacho chakula chochote hapa?” Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakichukua, akala, wote wakimwona. Halafu akawaambia, “Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: Kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi.” Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu. Akawaambia, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu, na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia Yerusalemu, yahubiriwe kwamba watu wanapaswa kutubu na kusamehewa dhambi. Nyinyi ni mashahidi wa mambo hayo. Nami mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi kumtuma, lakini ngojeni huku mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu.” Kisha akawaongoza nje ya mji hadi Bethania, akainua mikono yake juu, akawabariki. Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni. Wao wakamwabudu, kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa: Wakakaa muda wote hekaluni wakimsifu Mungu. Hapo mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu. Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu. Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye. Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu. Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda. Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane, ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini. Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote. Basi, Neno alikuwako ulimwenguni, na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua. Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu, ambao walizaliwa si kwa maumbile ya kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala mapenzi ya mtu, bali kutokana na Mungu mwenyewe. Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli. Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: ‘Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.’” Kutokana na ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema kupita neema. Maana Mungu alitoa sheria kwa njia ya Mose, nayo neema na kweli vimetujia kwa njia ya Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu. Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani na Walawi, wamwulize: “Wewe u nani?” Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.” Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Elia?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!” Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.” Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: ‘Sauti ya mtu anaita jangwani: Nyosheni njia ya Bwana.’” Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo. Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Masiha, wala Elia, wala yule nabii, mbona wabatiza?” Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado. Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.” Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ngambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza. Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyeongea juu yake niliposema: ‘Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!’ Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.” Yohane alishuhudia hivi: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake. Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma kubatiza watu kwa maji alikuwa ameniambia: ‘Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’ Mimi nimeona na nimeshuhudia kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.” Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili. Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazameni! Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu.” Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu. Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, “Mnatafuta nini?” Nao wakamjibu, “Rabi, (yaani Mwalimu), unakaa wapi?” Yesu akawaambia, “Njoni, nanyi mtaona.” Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu. Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, “Tumemwona Masiha” (maana yake Kristo). Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa” (Kigiriki ni Petro, yaani, “Mwamba”). Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.” Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro. Naye Filipo akamkuta Nathanaeli, akamwambia, “Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti.” Naye Nathanaeli akamwuliza Filipo, “Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.” Yesu alipomwona Nathanaeli akimjia, alisema juu yake, “Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: Hamna hila ndani yake.” Naye Nathanaeli akamwuliza, “Umepataje kunijua?” Yesu akamwambia, “Ulipokuwa chini ya mtini, hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona.” Hapo Nathanaeli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!” Yesu akamwambia, “Je, umeamini kwa kuwa nimekuambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya.” Yesu akaendelea kusema, “Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu.” Siku ya tatu kulikuwa na harusi mjini Kana, mkoani Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo, naye Yesu alikuwa amealikwa harusini pamoja na wanafunzi wake. Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, “Hawana divai!” Yesu akamjibu, “Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado.” Hapo mama yake akawaambia watumishi, “Lolote atakalowaambieni, fanyeni.” Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha. Yesu akawaambia, “Ijazeni mitungi hiyo maji.” Nao wakaijaza mpaka juu. Kisha akawaambia, “Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu.” Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi, akamwambia, “Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!” Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini. Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache. Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda juu Yerusalemu. Basi, akawakuta mle hekaluni watu wakiuza ng'ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao. Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya hekalu pamoja na kondoo na ng'ombe wao, akazitawanya sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao. Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, “Ondoeni vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!” Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: “Upendo wangu kwa nyumba yako waniua.” Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, “Utafanya mwujiza gani kuonesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?” Yesu akawaambia, “Vunjeni hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu.” Hapo Wayahudi wakasema, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arubaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?” Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya hekalu ambalo ni mwili wake. Basi, alipofufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakayaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno ambayo Yesu alikuwa amesema. Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizofanya. Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote. Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao. Kulikuwa na kiongozi mmoja Myahudi, wa kikundi cha Mafarisayo, jina lake Nikodemo. Siku moja Nikodemo alimwendea Yesu usiku, akamwambia, “Rabi, tunajua kwamba wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye.” Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, mtu asipozaliwa tena hataweza kuuona ufalme wa Mungu.” Nikodemo akamwuliza, “Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa tena!” Yesu akamjibu, “Kweli nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu. Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho. Usistaajabu kwamba nimekuambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya. Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho.” Nikodemo akamwuliza, “Mambo haya yanawezekanaje?” Yesu akamjibu, “Je, wewe ni mwalimu katika Israeli na huyajui mambo haya? Kweli nakuambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia tuliyoyaona, lakini nyinyi hamkubali ujumbe wetu. Ikiwa nimewaambieni mambo ya kidunia nanyi hamniamini, mtawezaje kuamini nikiwaambieni mambo ya mbinguni? Hakuna mtu aliyepata kwenda juu mbinguni isipokuwa Mwana wa Mtu, ambaye ameshuka kutoka mbinguni. “Kama vile Mose alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani, naye Mwana wa Mtu atainuliwa juu vivyo hivyo, ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele. Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali aukomboe. “Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa, kwa sababu hakumwamini Mwana wa pekee wa Mungu. Na hukumu yenyewe ndiyo hii: Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu. Kila mtu atendaye maovu anauchukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe. Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu.” Baada ya hayo, Yesu alifika mkoani Yudea pamoja na wanafunzi wake. Alikaa huko pamoja nao kwa muda, akibatiza watu. Yohane pia alikuwa akibatiza watu huko Ainoni, karibu na Salemu, maana huko kulikuwa na maji mengi. Watu walimwendea, naye akawabatiza. (Wakati huo Yohane alikuwa bado hajafungwa gerezani.) Ubishi ulitokea kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohane na Myahudi mmoja kuhusu desturi za kutawadha. Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia, “Mwalimu, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ngambo ya Yordani na ambaye wewe ulimshuhudia, sasa naye anabatiza, na watu wote wanamwendea.” Yohane akawaambia, “Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu. Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: ‘Mimi siye Kristo, lakini nimetumwa ili nimtangulie!’ Bibi arusi ni wake bwana arusi, lakini rafiki yake bwana arusi, anayesimama na kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana arusi akisema. Ndivyo furaha yangu ilivyokamilishwa. Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue.” Anayekuja kutoka juu ni mkuu kuliko wote; atokaye duniani ni wa dunia, na huongea mambo ya kidunia. Lakini anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wote. Yeye husema yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna mtu anayekubali ujumbe wake. Lakini mtu yeyote anayekubali ujumbe wake anathibitisha kwamba Mungu ni kweli. Yule aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, maana Mungu humjalia mtu huyo Roho wake bila kipimo. Baba anampenda Mwana na amemkabidhi vitu vyote. Anayemwamini Mwana anao uhai wa milele; asiyemwamini Mwana hatakuwa na uhai wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake. Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane. (Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.) Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya; na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria. Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu. Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana. Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, “Nipatie maji ninywe.” (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.) Lakini huyo mwanamke akamwambia, “Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?” (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu). Yesu akamjibu, “Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekuambia: ‘Nipatie maji ninywe,’ ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yenye uhai.” Huyo mama akasema, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yenye uhai? Au, labda wewe wajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo wake walikunywa maji ya kisima hiki.” Yesu akamjibu, “Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uhai na kumpatia uhai wa milele.” Huyo mwanamke akamwambia, “Bwana, nipe maji hayo ili nisione kiu tena; na, nisije tena mpaka hapa kuteka maji.” Yesu akamwambia, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.” Huyo mwanamke akamwambia, “Mimi sina mume.” Yesu akamwambia, “Umesema kweli, kwamba huna mume. Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli.” Huyo Mwanamke akamwambia, “Bwana, naona ya kuwa wewe u nabii. Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini nyinyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudia Mungu ni kule Yerusalemu.” Yesu akamwambia, “Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu. Nyinyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi. Lakini wakati waja, tena umekwisha wasili, ambapo wenye kuabudu wa kweli watamwabudu Baba katika roho na ukweli. Maana Baba anawataka watu wanaomwabudu namna hiyo. Mungu ni roho, na watu wanaomwabudu lazima wamwabudu kwa Roho na ukweli.” Huyo mama akamwambia, “Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu.” Yesu akamwambia, “Mimi ninayeongea nawe, ndiye.” Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: “Unataka nini?” au, “Kwa nini unaongea na mwanamke?” Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu, “Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?” Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu. Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: “Mwalimu, kula chakula.” Lakini Yesu akawaambia, “Mimi ninacho chakula msichokijua nyinyi.” Wanafunzi wake wakaulizana, “Je, kuna mtu aliyemletea chakula?” Yesu akawaambia, “Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake. Nyinyi mwasema: ‘Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!’ Lakini mimi nawaambieni, angalieni mkaone jinsi mashamba yalivyo tayari kuvunwa. Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uhai wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja. Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna.’ Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho; wengine walifanya kazi, lakini nyinyi mnafaidika kutokana na jasho lao.” Wasamaria wengi wa kijiji kile walimwamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: “Ameniambia mambo yote niliyofanya.” Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili. Watu wengi zaidi waliamini kwa sababu ya ujumbe wake. Wakamwambia yule mama, “Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu.” Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya. Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, “Nabii hapati heshima katika nchi yake.” Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo. Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu. Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi. Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!” Huyo ofisa akamwambia, “Bwana, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa.” Yesu akamwambia, “Nenda tu, mwanao ataishi.” Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake. Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima. Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, “Jana saa saba mchana, homa ilimwacha.” Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: “Mwanao ataishi.” Hapo yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote. Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda Galilaya. Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu. Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye matao. Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: Vipofu, viwete na waliopooza. [Walikuwa wakingojea maji yatibuliwe, maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.] Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane. Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo na kujua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, “Je, wataka kupona?” Naye akajibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia.” Yesu akamwambia, “Inuka, chukua mkeka wako utembee.” Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato. Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia huyo mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato, si halali kubeba mkeka wako.” Lakini yeye akawaambia, “Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia: ‘Chukua mkeka wako, utembee.’” Nao wakamwuliza, “Huyo mtu aliyekuambia: ‘Chukua mkeka wako, utembee,’ ni nani?” Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu. Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa hekaluni, akamwambia, “Sasa umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi.” Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye aliyemponya. Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza kumdhulumu. Basi, Yesu akawaambia, “Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia nafanya kazi.” Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya kumuua Yesu; si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu. Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya Baba, Mwana hukifanya vilevile. Baba ampenda Mwana, na humwonesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena atamwonesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu. Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uhai, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uhai wale anaopenda. Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana, ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma. “Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uhai wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifoni na kuingia katika uhai. Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi. Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai. Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu. Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake, nao watafufuka: Wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa. “Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi ninahukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma. Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli. Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli. Nyinyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli. Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa. Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo. Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma. Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Nyinyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake, na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma. Nyinyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uhai wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia! Hata hivyo, nyinyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uhai. “Shabaha yangu si kupata sifa kutoka kwa watu. Lakini nawajua nyinyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu. Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea. Mwawezaje kuamini, hali nyinyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu nyinyi wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu? Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye nyinyi mmemtumainia ndiye atakayewashtaki. Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia, maana Mose aliandika juu yangu. Lakini hamyaamini yale aliyoandika; mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?” Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au ziwa Tiberia). Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa. Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake. Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia. Basi, Yesu alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia Filipo, “Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?” (Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.) Filipo akamjibu, “Mikate ya fedha dinari 200 haiwatoshi watu hawa hata kama kila mmoja atapata kipande kidogo tu!” Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, “Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?” Yesu akasema, “Waketisheni watu.” Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume 5,000. Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka. Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee.” Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili. Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, “Hakika huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni.” Yesu akajua kwamba watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, akaenda mlimani peke yake. Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani, wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado. Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana. Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope!” Basi wakataka kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu walikokuwa wanakwenda. Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua pamoja na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke yao. Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu. Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta. Wale watu walipomkuta Yesu ngambo ya pili wa ziwa walimwuliza, “Mwalimu, ulifika lini hapa?” Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishughulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uhai wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho.” Wao wakamwuliza, “Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?” Yesu akawajibu, “Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu mwifanye: Kumwamini yule aliyemtuma.” Hapo wakamwambia, “Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya kitu gani? Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: ‘Aliwalisha mkate kutoka mbinguni.’” Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye nyinyi mkate wa kweli kutoka mbinguni. Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uhai.” Basi, wakamwambia, “Bwana, tupe daima mkate huo.” Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe. Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini. Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami kamwe sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu, kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma. Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: Nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote siku ya mwisho. Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: Kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uhai wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.” Basi, Wayahudi wakaanza kunungunika kwa kuwa alisema: “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunamjua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?” Yesu akawaambia, “Acheni kunungunika nyinyi kwa nyinyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo siku ya mwisho. Manabii wameandika: ‘Watu wote watafundishwa na Mungu.’ Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu. Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uhai wa milele. Mimi ni mkate wa uhai. Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa. Lakini huu ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni ili yeyote atakayeula asife. Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uhai wa ulimwengu.” Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: “Anawezaje huyu kutupa mwili wake, tule?” Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu. Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uhai wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho. Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake. Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu. Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu zenu, wakafa. Aulaye mkate huu atakuwa hai milele.” Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu. Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, “Haya ni mambo magumu! Nani awezaye kuyasikiliza?” Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananungunika juu ya jambo hilo, akawauliza, “Je, jambo hili linawafanya muwe na mashaka? Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa kwanza? Roho ndiyo iletayo uhai; mwili hauwezi kitu. Maneno niliyowaambia ni roho na uhai. Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini.” (Yesu alisema hivyo kwani alijua tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti). Kisha akasema, “Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu.” Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma, wasiandamane naye tena. Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, “Je, nanyi pia mwataka kwenda zenu?” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno ya uhai wa milele. Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu” Yesu akawaambia, “Je, sikuwachagua nyinyi kumi na wawili? Hata hivyo, mmoja wenu ni Ibilisi!” Yesu alisema hayo juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyu alikuwa ndiye atakayemsaliti, ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili. Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea huko Galilaya. Hakutaka kutembea mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa wanataka kumuua. Sikukuu ya Wayahudi ya vibanda ilikuwa imekaribia. Basi, ndugu zake wakamwambia, “Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya. Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadamu unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu.” (Hata ndugu zake hawakumwamini). Basi, Yesu akawaambia, “Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini kwenu nyinyi kila wakati unafaa. Ulimwengu hauwezi kuwachukia nyinyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi nashuhudia juu yake kwamba matendo yake ni maovu. Nyinyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika.” Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya. Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri. Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; wakauliza, “Yuko wapi?” Kulikuwa na minongono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walisema, “La! Anawapotosha watu.” Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi. Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda hekaluni, akaanza kufundisha. Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema, “Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?” Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma. Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe. Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote. Je, Mose hakuwapeni sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” Hapo watu wakamjibu, “Una pepo wewe! Nani anataka kukuua?” Yesu akawajibu, “Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia. Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa nyinyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato. Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi sheria isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato? Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki.” Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, “Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu? Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo? Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!” Basi, Yesu alipokuwa anafundisha hekaluni alipaza sauti na kusema, “Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui. Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.” Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, “Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?” Mafarisayo waliwasikia watu wakinongona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni. Yesu akasema, “Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma. Mtanitafuta lakini hamtaniona, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika.” Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, “Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki? Ana maana gani anaposema: ‘Mtanitafuta lakini hamtanipata, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika?’” Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalumu. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, “Aliye na kiu na aje kwangu anywe. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: ‘Anayeniamini mimi, mito ya maji ya uhai itatiririka kutoka moyoni mwake!’” (Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado). Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, “Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!” Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine walisema, “Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya? Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: ‘Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!’” Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu. Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata. Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, “Kwa nini hamkumleta?” Walinzi wakawajibu, “Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!” Mafarisayo wakawauliza, “Je, nanyi pia mmedanganyika? Je, mmekwisha kumwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini? Lakini umati huu haujui sheria ya Mose; umelaaniwa!” Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia, “Je, sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?” Nao wakamjibu, “Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!” [ Basi, wote wakaondoka, kila mtu akaenda nyumbani; Lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni. Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha. Basi, waalimu wa sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao. Kisha wakamwuliza Yesu, “Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi. Katika sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?” Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole. Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, “Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe.” Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini. Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitangulia wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale. Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, “Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?” Huyo mwanamke akamjibu, “Bwana, hakuna hata mmoja!” Naye Yesu akamwambia, “Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena.”] Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uhai.” Basi, Mafarisayo wakamwambia, “Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali.” Yesu akawajibu, “Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini nyinyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda. Nyinyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu. Hata nikihukumu, hukumu yangu ni halali kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami. Imeandikwa katika sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali. Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia.” Hapo wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu, “Nyinyi hamnijui mimi wala hammjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia.” Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. Yesu akawaambia tena, “Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, nyinyi hamwezi kufika.” Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Mbona anasema: ‘Niendako nyinyi hamwezi kufika?’” Yesu akawaambia, “Nyinyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; nyinyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba ‘Mimi Ndimi Niliye’, mtakufa katika dhambi zenu.” Nao wakamwuliza, “Wewe ni nani?” Yesu akawajibu, “Nimewaambieni tangu mwanzo! Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake.” Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba. Basi, Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu, hapo ndipo mtakapojua kwamba ‘Mimi Ndimi Niliye’, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha. Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza.” Baada ya kusema hayo watu wengi walimwamini. Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu. Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru.” Nao wakamjibu, “Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: ‘Mtakuwa huru?’” Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi. Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu. Mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli. Najua kwamba nyinyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamyakubali mafundisho yangu. Mimi nasema yale aliyonionesha Baba, lakini nyinyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu.” Wao wakamjibu, “Sisi ni watoto wa Abrahamu!” Yesu akawaambia, “Kama nyinyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu. Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, nyinyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo! Nyinyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya baba yenu.” Wao wakamwambia, “Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu.” Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. Kwa nini hamuelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu. Nyinyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo. Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana nyinyi hamniamini. Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini? Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini nyinyi hamsikilizi kwa sababu nyinyi si watu wa Mungu.” Wayahudi wakamwambia, “Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?” Yesu akajibu, “Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini nyinyi hamniheshimu. Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu. Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele.” Basi, Wayahudi wakasema, “Sasa tunajua kweli kwamba wewe una pepo! Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, ‘Anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele!’ Je, unajifanya mkuu kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?” Yesu akawajibu, “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu ambaye nyinyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza. Nyinyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama nyinyi. Mimi namjua na ninashika neno lake. Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi.” Basi, Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona Abrahamu?” Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko.” Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni. Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa. Basi, wanafunzi wakamwuliza, “Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: Mtu huyu, ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?” Yesu akajibu, “Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake. Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi. Wakati ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu.” Baada ya kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule kipofu machoni, akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Maana ya jina hili ni “aliyetumwa”). Hapo, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha akarudi akiwa anaona. Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini mwombaji, wakasema, “Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?” Baadhi yao wakasema, “Ndiye.” Wengine wakasema, “La! Ila anafanana naye.” Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, “Ni mimi!” Basi, wakamwuliza, “Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?” Naye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na kuniambia: ‘Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.’ Hapo, mimi nikaenda, nikanawa, nikapata kuona.” Wakamwuliza, “Yeye yuko wapi?” Naye akawajibu, “Mimi sijui!” Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo. Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato. Basi, Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, “Umepataje kuona?” Naye akawaambia, “Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona.” Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki sheria ya Sabato.” Lakini wengine wakasema, “Mtu mwenye dhambi awezaje kufanya ishara za namna hii?” Kukawa na mafarakano kati yao. Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, “Maadamu yeye amekufungua macho, wasemaje juu yake?” Naye akawaambia, “Yeye ni nabii!” Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na sasa anaona, mpaka walipowaita wazazi wake. Basi, wakawauliza hao wazazi, “Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye nyinyi mwasema alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?” Wazazi wake wakajibu, “Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa kipofu. Lakini amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe.” Wazazi wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani viongozi hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu ni Kristo atafukuzwa nje ya sunagogi. Ndiyo maana wazazi wake walisema: “Yeye ni mtu mzima, mwulizeni.” Basi, wakamwita tena huyo aliyekuwa kipofu, wakamwambia, “Sema ukweli mbele ya Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi.” Yeye akajibu, “Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua: Nilikuwa kipofu, na sasa naona.” Basi, wakamwuliza, “Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?” Huyo mtu akawajibu, “Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini mwataka kusikia tena? Je, nyinyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?” Lakini wao wakamtukana wakisema, “Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa Mose. Sisi tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka wapi!” Naye akawajibu, “Hili ni jambo la kushangaza! Nyinyi hamjui ametoka wapi, lakini amenifumbua macho yangu! Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote mwenye kumcha na kutimiza mapenzi yake. Tangu mwanzo wa ulimwengu haijasikika kwamba mtu ameyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu. Kama mtu huyu hakutoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote!” Wao wakamjibu, “Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje kutufundisha sisi?” Basi, wakamfukuza sunagogini. Yesu alisikia kwamba walikuwa wamemfukuza sunagogini. Basi, alipomkuta akamwuliza, “Je, wewe unamwamini Mwana wa Mtu?” Huyo mtu akajibu, “Mheshimiwa, niambie yeye ni nani, ili nipate kumwamini.” Yesu akamwambia, “Umekwisha mwona, naye ndiye anayesema nawe sasa.” Basi, huyo mtu akasema, “Ninaamini Bwana!” Akamsujudia. Yesu akasema, “Mimi nimekuja ulimwenguni kutoa hukumu, kusudi wasioona wapate kuona, na wale wanaoona wawe vipofu.” Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye walisikia maneno hayo, wakamwuliza, “Je, sisi pia ni vipofu?” Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia; lakini sasa nyinyi mwasema: ‘Sisi tunaona,’ na hiyo yaonesha kwamba mna hatia bado. “Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyanganyi. Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo. Mngojamlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake, na kuwaongoza nje. Akisha watoa nje huwatangulia mbele, nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake. Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake.” Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia. Basi, akasema tena, “Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo. Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyanganyi, nao kondoo hawakuwasikiliza. Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho. Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uhai — uhai kamili. “Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwamwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia, kisha mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu. Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi, kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao. Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. “Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena. Hakuna mtu anayeninyanganya uhai wangu; mimi nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye.” Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya. Wengi wao wakasema, “Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?” Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?” Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi. Naye Yesu akawa anatembea hekaluni katika ukumbi wa Solomoni. Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, “Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiwe Kristo, basi, tuambie wazi.” Yesu akawajibu, “Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia. Lakini nyinyi hamsadiki kwa sababu nyinyi si kondoo wangu. Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata. Mimi nawapa uhai wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wala hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba. Mimi na Baba, tu mmoja.” Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie. Yesu akawaambia, “Nimewaonesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?” Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa ajili ya kazi njema, ila kwa sababu ya kumkufuru Mungu! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu.” Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika sheria yenu: ‘Mimi nimesema, nyinyi ni miungu?’ Mungu aliwaita miungu wale waliopewa ujumbe wake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima. Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: ‘Unakufuru,’ eti kwa sababu nilisema: ‘Mimi ni Mwana wa Mungu?’ Kama sifanyi kazi za Baba yangu, msiniamini. Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi, mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake.” Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao. Yesu akaenda tena ngambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko. Watu wengi walimwendea wakasema, “Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa.” Watu wengi mahali hapo wakamwamini. Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake. Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa). Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: “Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!” Yesu aliposikia hivyo, akasema, “Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe.” Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro. Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi. Kisha akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni tena Yudea!” Wanafunzi wakamwambia, “Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?” Yesu akajibu, “Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu. Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake.” Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, ikiwa amelala, basi atapona.” Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro. Basi, Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa; lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake.” Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Twendeni nasi tukafe pamoja naye!” Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne. Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu, umbali upatao kilomita tatu. Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao. Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani. Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa! Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.” Yesu akamwambia, “Kaka yako atafufuka.” Martha akamjibu, “Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho.” Yesu akamwambia, “Mimi ndimi ufufuo na uhai. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi; na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?” Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana! Mimi naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.” Baada ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwambia faraghani, “Mwalimu yuko hapa, anakuita.” Naye aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu. Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha alipomlaki. Basi, Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona ameinuka na kutoka nje ghafla, walimfuata. Walidhani alikuwa anakwenda kaburini kuomboleza. Basi, Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti, akamwambia, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!” Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, alijawa na huzuni na kufadhaika moyoni. Kisha akawauliza, “Mlimweka wapi?” Wakamwambia, “Bwana, njoo uone.” Yesu akalia machozi. Basi, Wayahudi wakasema, “Tazameni jinsi alivyompenda!” Lakini baadhi yao wakasema, “Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya Lazaro asife?” Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe. Yesu akasema, “Ondoeni hilo jiwe!” Martha, dada yake huyo aliyekufa, akamwambia, “Bwana, amekwisha anza kunuka; amekaa kaburini siku nne!” Yesu akamwambia, “Je, sikukuambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?” Basi, wakaliondoa lile jiwe. Yesu akatazama juu mbinguni, akasema, “Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza. Najua kwamba unanisikiliza daima. Lakini nimesema hayo kwa ajili ya watu hawa waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma.” Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa: “Lazaro! Toka nje!” Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda miguu na mikono, na uso wake umefunikwa. Yesu akawaambia, “Mfungueni, mkamwache aende zake.” Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria walipoona kitendo hicho alichokifanya Yesu, wakamwamini. Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa taarifa ya jambo hilo alilofanya Yesu. Kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza Kuu, wakasema, “Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno. Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu hekalu letu na taifa letu!” Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, akawaambia, “Nyinyi hamjui kitu! Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa zima liangamizwe?” Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa vile alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa lao; na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika. Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya mipango ya kumwua Yesu. Kwa hiyo, Yesu hakutembea tena hadharani kati ya Wayahudi, bali alitoka hapo, akaenda mahali karibu na jangwa, katika mji uitwao Efraimu. Akakaa huko pamoja na wanafunzi wake. Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa karibu, na watu wengi walikwenda Yerusalemu ili wajitakase kabla ya sikukuu hiyo. Basi, wakawa wanamtafuta Yesu. Nao walipokusanyika pamoja hekaluni, wakaulizana, “Mwaonaje? Yaonekana kwamba haji kabisa kwenye sikukuu, au sivyo?” Makuhani wakuu na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kwamba mtu akijua mahali aliko Yesu awaarifu kusudi wamtie nguvuni. Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu. Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu. Basi, Maria alichukua nusu lita ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi. Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema, “Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari 300, wakapewa maskini?” Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina. Lakini Yesu akasema, “Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote.” Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka kwa wafu. Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro, maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu. Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu. Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaza sauti wakisema: “Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli.” Yesu akampata mwanapunda mmoja, akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko: “Usiogope mji wa Siyoni! Tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwanapunda!” Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo. Kundi la watu wale waliokuwa pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka kwa wafu, walimshuhudia. Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo. Basi, Mafarisayo wakaambiana, “Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata.” Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo. Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, “Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu.” Filipo akaenda, akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu. Yesu akawaambia, “Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika! Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi. Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uhai wa milele. Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima. “Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: ‘Baba, usiruhusu saa hii inifikie?’ Lakini ndiyo maana nimekuja — ili nipite katika saa hii. Baba, ulitukuze jina lako.” Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, na nitalitukuza tena.” Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, “Ni ngurumo.” Lakini wengine wakasema, “Malaika ameongea naye!” Lakini Yesu akawaambia, “Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu. Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa. Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu.” (Kwa kusema hivyo alionesha atakufa kifo gani). Basi, umati huo ukamjibu, “Sisi tunaambiwa na sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?” Yesu akawaambia, “Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako. Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga.” Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao. Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini. Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: “Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?” Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya alisema tena: “Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate kuwaponya.” Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake. Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi. Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu. Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, “Mtu anayeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma. Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma. Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani. Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki, mimi sitamhukumu; maana sikuja kuuhukumu ulimwengu bali kuuokoa. Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: Neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho. Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini. Nami najua kuwa amri yake huleta uhai wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme.” Ilikuwa siku kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua kwamba saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa amewapenda daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho! Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa wamekaa kula chakula cha jioni. Ibilisi alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya kumsaliti Yesu. Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu. Basi, aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia. Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, “Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?” Yesu akamjibu, “Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye.” Petro akamwambia, “Wewe hutaniosha miguu kamwe!” Yesu akamjibu, “Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami tena.” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na kichwa pia.” Yesu akamwambia, “Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Nyinyi mmetakata, lakini si nyote.” ( Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: “Nyinyi mmetakata, lakini si nyote.”) Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, “Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni? Nyinyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi. Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu nimewaosha nyinyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu. Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni. Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu kuliko yule aliyemtuma. Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza. “Haya nisemayo hayawahusu nyinyi nyote. Mimi nawajua wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: ‘Yule aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.’ Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa ‘Mimi Ndimi.’ Kweli nawaambieni: Anayempokea yule ninayemtuma ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma.” Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!” Wanafunzi wakatazamana wasiweze kabisa kujua anamsema nani. Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu. Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: “Mwulize anasema juu ya nani.” Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, “Bwana, ni nani?” Yesu akajibu, “Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye.” Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti. Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, “Unachotaka kufanya, kifanye haraka!” Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo. Kwa kuwa Yuda alikuwa mweka hazina, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini. Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate, akatoka nje mara. Na ilikuwa usiku. Baada ya Yuda kuondoka, Yesu akasema, “Sasa Mwana wa Mtu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. Na kama utukufu wa Mungu umefunuliwa ndani ya Mwana, basi, naye Mungu ataudhihirisha utukufu wa Mwana ndani yake mwenyewe, na atafanya hivyo mara. “Watoto wangu, bado niko nanyi kwa muda mfupi tu. Mtanitafuta, lakini sasa nawaambieni yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: ‘Niendako nyinyi hamwezi kwenda!’ Nawapeni amri mpya: Pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda nyinyi. Mkipendana, watu wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu.” Simoni Petro akamwuliza, “Bwana, unakwenda wapi?” Yesu akajibu, “Niendako huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye.” Petro akamwambia “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Niko tayari kufa kwa ajili yako!” Yesu akajibu, “Je, uko tayari kweli kufa kwa ajili yangu? Kweli nakuambia, kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu!” Yesu aliwaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama isingekuwa hivyo, ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi. Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi. Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda.” Thoma akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?” Yesu akamjibu, “Mimi ni njia, na ukweli na uhai. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu. Ikiwa mnanijua mimi, mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona.” Filipo akamwambia, “Bwana, tuoneshe Baba, nasi tutatosheka.” Yesu akamwambia, “Nimekaa nanyi muda wote huu, nawe Filipo hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: ‘Tuoneshe Baba?’ Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake. Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya. Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, kwani ninakwenda kwa Baba. Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni. “Mkinipenda mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele. Yeye ni Roho wa ukweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini nyinyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu. “Sitawaacha nyinyi yatima; nitakuja tena kwenu. Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini nyinyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai. Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu. Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, “Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?” Yesu akamjibu, “Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye. Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma. “Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi, lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni. “Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike. Mlikwisha sikia nikiwaambieni: ‘Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.’ Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi. Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini. Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu; lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa! “Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda yeye huliondoa, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi. Nyinyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni. Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipobaki katika mzabibu, hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. “Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami nikiwa ndani yake, huyo huzaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote. Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue. Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa. Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu. Mimi nimewapenda nyinyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike. Hii ndiyo amri yangu: Pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda nyinyi. Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Nyinyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. Nyinyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita nyinyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu. Nyinyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapeni chochote mnachomwomba kwa jina langu. Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: Pendaneni. “Kama ulimwengu ukiwachukia nyinyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla ya kuwachukia nyinyi. Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda nyinyi kama watu wake. Lakini kwa vile nyinyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni. Kumbukeni niliyowaambieni: Mtumishi si mkuu kuliko bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na nyinyi pia; kama wameshika neno langu, watalishika na lenu pia. Lakini hayo yote watawatendeeni nyinyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma. Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi. Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia. Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine amekwisha yafanya wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya wakanichukia mimi, wakamchukia na Baba yangu pia. Ndiyo maana yale yaliyoandikwa katika sheria yao ni kweli: ‘Wamenichukia bure!’ “Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, huyo Roho wa ukweli, atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu mwanzo. “Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu. Watu watawafukuza nyinyi katika masunagogi yao. Tena, wakati unakuja ambapo kila atakayewaua nyinyi atadhani anamhudumia Mungu. Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi. Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba niliwaambieni. “Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi. Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: ‘Unakwenda wapi?’ Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu. Lakini, nawaambieni ukweli: Afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu. Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu. Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini; kuhusu uadilifu, kwa sababu nakwenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena; kuhusu hukumu, kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa. “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili. Lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atasema atakayoyasikia na kuwajulisheni yatakayokuja. Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawajulisheni yale atakayopata kutoka kwangu. Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho atawajulisheni yale atakayopata kutoka kwangu. “Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!” Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, “Ana maana gani anapotuambia: ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?’ Tena anasema: ‘Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!’” Basi, wakawa wanaulizana, “Ana maana gani anaposema: ‘Bado kitambo kidogo?’ Hatuelewi anasema nini.” Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, “Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?’ Nawaambieni kweli, nyinyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi; mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani. Nyinyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu. Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni. Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu ikamilike. “Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba. Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu; maana yeye mwenyewe anawapenda nyinyi, kwa sababu nyinyi mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba.” Basi, wanafunzi wake wakamwambia, “Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo. Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu.” Yesu akawajibu, “Je, mnaamini sasa? Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo nyinyi nyote mtatawanywa kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami. Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!” Yesu alipokwisha sema hayo, alitazama juu mbinguni, akasema, “Baba, ile saa imefika! Mtukuze Mwanao ili naye Mwana apate kukutukuza. Maana ulimpa Mwanao mamlaka juu ya watu wote ili awape uhai wa milele wote hao uliompa. Na uhai wa milele ndio huu: Kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli, na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma. Mimi nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha ile kazi uliyonipa niifanye. Sasa, Baba, nitukuze mbele yako kwa ule utukufu niliokuwa nao kabla ya kuumbwa ulimwengu. “Nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa kutoka duniani. Walikuwa watu wako, nawe ukanipa wawe wangu; nao wamelishika neno lako. Sasa wanajua kwamba kila ulichonipa kimetoka kwako. Mimi nimewapa ule ujumbe ulionipa, nao wameupokea; wanajua kwamba kweli nimetoka kwako, na wanaamini kwamba wewe ulinituma. “Nawaombea hao; siuombei ulimwengu, ila nawaombea wale ulionipa, maana ni wako. Yote niliyo nayo ni yako, na yako ni yangu; na utukufu wangu umeonekana katika hao ulionipa. Na sasa naja kwako; simo tena ulimwenguni, lakini wao wamo ulimwenguni. Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulilonipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja. Nilipokuwa nao, mimi niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Mimi nimewalinda, wala hakuna hata mmoja wao aliyepotea, isipokuwa yule mwana mpotevu, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia. Basi, sasa naja kwako, na nimesema mambo haya ulimwenguni, ili waweze kushiriki kikamilifu furaha yangu. Mimi nimewapa ujumbe wako, nao ulimwengu ukawachukia, kwa sababu wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu. Siombi uwatoe ulimwenguni, bali naomba uwakinge na yule Mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu. Waweke wakfu katika ukweli; neno lako ni ukweli. Kama vile ulivyonituma ulimwenguni, nami pia nimewatuma wao ulimwenguni; na kwa ajili yao mimi mwenyewe najiweka wakfu ili nao pia wafanywe wakfu katika ukweli. “Siwaombei hao tu, bali nawaombea pia wote watakaoamini kutokana na ujumbe wao. Naomba ili wote wawe kitu kimoja. Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma. Mimi nimewapa utukufu uleule ulionipa mimi, ili wawe kitu kimoja kama nasi tulivyo mmoja; mimi niwe ndani yao, nawe uwe ndani yangu; naomba wakamilishwe na kuwa kitu kimoja, ili ulimwengu upate kujua kwamba wewe ulinituma, na kwamba unawapenda wao kama unavyonipenda mimi. “Baba! Nataka hao ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili wauone utukufu wangu ulionipa; kwa kuwa ulinipenda kabla ya kuumbwa ulimwengu. Baba Mwema! Ulimwengu haukujui, lakini mimi nakujua. Hawa nao wanajua kwamba wewe ulinituma. Nimekufanya ujulikane kwao na nitaendelea kufanya hivyo, ili upendo ulio nao kwangu uwe ndani yao, nami niwe ndani yao.” Yesu alipokwisha sema hayo, alikwenda ngambo ya kijito Kedroni, pamoja na wanafunzi wake. Mahali hapo palikuwa na bustani, naye Yesu akaingia humo pamoja na wanafunzi wake. Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipajua mahali hapo kwani mara nyingi Yesu alikutana na wanafunzi wake huko. Basi, Yuda alichukua kikosi cha askari na walinzi kutoka kwa makuhani wakuu na Mafarisayo, akaja nao bustanini wakiwa na taa, mienge na silaha. Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawauliza, “Mnamtafuta nani?” Nao wakamjibu, “Yesu Mnazareti!” Yesu akawaambia, “Mimi ndiye.” Msaliti Yuda alikuwa amesimama hapo pamoja nao. Basi, Yesu alipowaambia: “Mimi ndiye,” wakarudi nyuma, wakaanguka chini. Yesu akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?” Wakamjibu, “Yesu Mnazareti!” Yesu akawaambia, “Nimekwisha waambieni kwamba mimi ndiye. Basi, kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.” ( Alisema hayo ili yapate kutimia yale aliyosema: “Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja.”) Simoni Petro alikuwa na upanga; basi, akauchomoa, akamkata sikio la kulia mtumishi wa kuhani mkuu. Mtumishi huyo aliitwa Malko. Basi, Yesu akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako alani. Je, nisinywe kikombe cha mateso alichonipa Baba?” Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe wa Kayafa ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo. Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu. Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata Yesu. Huyo mwanafunzi mwingine alikuwa anajulikana kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia pamoja na Yesu ndani ya ukumbi wa kuhani mkuu. Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango. Basi, huyo mwanafunzi mwingine aliyekuwa anajulikana kwa kuhani mkuu alitoka nje akasema na mjakazi, mngojamlango, akamwingiza Petro ndani. Huyo mjakazi mngojamlango akamwuliza Petro, “Je, nawe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?” Petro akamwambia, “Si mimi!” Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu kulikuwa na baridi, wakawa wanaota moto. Naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto. Basi, kuhani mkuu akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho yake. Yesu akamjibu, “Nimesema na kila mtu daima hadharani. Kila mara nimefundisha katika masunagogi na hekaluni, mahali wanapokutana Wayahudi wote; na wala sijasema chochote kwa siri. Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini niliwaambia. Wao wanajua niliyowaambia.” Alipokwisha sema hayo mlinzi mmoja aliyekuwa amesimama hapo akampiga kofi akisema, “Je, ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?” Yesu akamjibu, “Kama nimesema vibaya, onesha huo ubaya; lakini ikiwa nimesema vema, mbona wanipiga?” Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa kuhani mkuu Kayafa. Petro alikuwa hapo akiota moto. Basi, wakamwuliza, “Je, nawe pia si mmoja wa wanafunzi wake?” Yeye akakana na kusema, “Si mimi!” Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, jamaa wa yule aliyekatwa sikio na Petro, akamwuliza, “Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?” Petro akakana tena; mara jogoo akawika. Basi, walimchukua Yesu kutoka kwa Kayafa, wakampeleka ikulu. Ilikuwa alfajiri, nao ili waweze kula Pasaka, hawakuingia ndani ya ikulu wasije wakatiwa unajisi. Kwa hiyo, Pilato aliwaendea nje, akasema, “Mna mashtaka gani juu ya mtu huyu?” Wakamjibu, “Kama huyu hangalikuwa mwovu hatungalimleta kwako.” Pilato akawaambia, “Haya, mchukueni nyinyi wenyewe, mkamhukumu kufuatana na sheria yenu.” Wayahudi wakamjibu, “Sisi hatuna mamlaka ya kumwua mtu yeyote.” ( Ilifanyika hivyo yapate kutimia maneno aliyosema Yesu kuonesha atakufa kifo gani.) Pilato akaingia tena ndani ya ikulu, akamwita Yesu na kumwuliza: “Ati wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamjibu, “Je, hayo ni maneno yako au wengine wamekuambia habari zangu?” Pilato akamjibu, “Je, ni Myahudi mimi? Taifa lako na makuhani wamekuleta kwangu. Umefanya nini?” Yesu akamjibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini sasa ufalme wangu si wa hapa.” Hapo Pilato akamwambia, “Basi, wewe ni Mfalme?” Yesu akajibu, “Wewe umesema kwamba mimi ni Mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili hiyo; na kwa ajili hiyo nimekuja ulimwenguni kuwaambia watu juu ya ukweli. Kila mtu wa ukweli hunisikiliza.” Pilato akamwambia, “Ukweli ni kitu gani?” Pilato alipokwisha sema hayo, aliwaendea tena Wayahudi nje, akawaambia, “Mimi sioni hatia yoyote kwake. Lakini, mnayo desturi kwamba mimi niwafungulie mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Basi, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?” Hapo wakapiga kelele: “La! Si huyu ila Baraba!” Naye Baraba alikuwa mnyanganyi. Basi, Pilato akaamuru Yesu achukuliwe, apigwe viboko. Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika na joho la rangi ya zambarau. Wakawa wanakuja mbele yake na kusema: “Shikamoo, Mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga makofi. Pilato akatoka nje tena, akawaambia, “Tazameni, namleta nje kwenu, mpate kujua kwamba mimi sikuona hatia yoyote kwake.” Basi, Yesu akatoka nje amevaa taji ya miiba na joho la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni! Mtu mwenyewe ni huyo.” Makuhani wakuu na walinzi walipomwona wakapaza sauti: “Msulubishe! Msulubishe!” Pilato akawaambia, “Mchukueni basi, nyinyi wenyewe mkamsulubishe, kwa maana mimi sikuona hatia yoyote kwake.” Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria, na kufuatana na sheria hiyo, ni lazima afe, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.” Pilato aliposikia maneno hayo akazidi kuogopa. Basi, akaingia ndani ya ikulu tena, akamwuliza Yesu, “Umetoka wapi wewe?” Lakini Yesu hakumjibu neno. Hivyo Pilato akamwambia, “Husemi nami? Je, hujui kwamba ninayo mamlaka ya kukufungua na mamlaka ya kukusulubisha?” Yesu akamjibu, “Hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa na Mungu. Kwa sababu hiyo, yule aliyenikabidhi kwako ana dhambi kubwa zaidi.” Tangu hapo, Pilato akawa anatafuta njia ya kumwachilia, lakini Wayahudi wakapiga kelele: “Ukimwachilia huyu mtu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu anayejifanya kuwa mfalme humpinga Kaisari!” Basi, Pilato aliposikia maneno hayo akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo “Sakafu ya Mawe” (kwa Kiebrania, Gabatha). Ilikuwa yapata saa sita mchana, siku ya maandalio ya Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, “Tazameni, Mfalme wenu!” Wao wakapaza sauti: “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe Mfalme wenu?” Makuhani wakuu wakajibu, “Sisi hatuna mfalme isipokuwa Kaisari!” Hapo, Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulubiwe. Basi, wakamchukua Yesu. Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo “Fuvu la Kichwa” (kwa Kiebrania Golgotha). Hapo ndipo walipomsulubisha, na pamoja naye waliwasulubisha watu wengine wawili; mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto, naye Yesu katikati. Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba. Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: “Yesu Mnazareti, Mfalme wa Wayahudi.” Wayahudi wengi waliisoma ilani hiyo, maana mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji. Tena ilani hiyo ilikuwa imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki. Basi, makuhani wakuu wakamwambia Pilato, “Usiandike: ‘Mfalme wa Wayahudi,’ ila ‘Yeye alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’” Pilato akajibu, “Niliyoandika, nimeandika!” Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa mafungu manne, fungu moja kwa kila askari. Walichukua pia na kanzu yake; kanzu hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono. Basi, hao askari wakashauriana: “Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya nani.” Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: “Waligawana mavazi yangu, na nguo yangu wakaipigia kura.” Basi, ndivyo walivyofanya hao askari. Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene. Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake, “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.” Halafu akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake. Kisha, Yesu aliona kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, “Naona kiu.” Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni. Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, “Yametimia!” Kisha akainamisha kichwa, akatoa roho. Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio. Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe na miili yao iondolewe. Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu. Lakini walipomfikia Yesu, waliona kwamba alikwisha kufa, kwa hivyo hawakumvunja miguu. Lakini askari mmoja alimtoboa ubavuni kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji. ( Naye aliyeona tukio hilo ameshuhudia ili nanyi mpate kuamini. Na hayo aliyosema ni ukweli, tena yeye anajua kwamba anasema ukweli). Jambo hilo lilitendwa ili Maandiko Matakatifu yatimie: “Hapana hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.” Tena Maandiko mengine yanasema: “Watamtazama yule waliyemtoboa.” Baada ya hayo, Yosefu, mwenyeji wa Arimathaya, alimwomba Pilato ruhusa ya kuuchukua mwili wa Yesu. (Yosefu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini kwa siri, maana aliwaogopa viongozi wa Wayahudi). Basi, Pilato akamruhusu. Hivyo Yosefu alikwenda, akauondoa mwili wa Yesu. Naye Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu usiku, akaja akiwa amechukua mchanganyiko wa manemane na ubani kiasi cha kilo thelathini. Basi, waliutwaa mwili wa Yesu, wakaufunga sanda pamoja na manukato kufuatana na desturi ya Wayahudi katika kuzika. Mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa na bustani, na katika bustani hiyo kulikuwa na kaburi jipya ambalo hakutiwa bado mtu yeyote ndani yake. Basi, kwa sababu ya shughuli za Wayahudi za maandalio ya Sabato, na kwa vile kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamweka Yesu humo. Alfajiri na mapema Jumapili, kukiwa bado na giza, Maria Magdalene alikwenda kaburini, akaliona lile jiwe limeondolewa mlangoni pa kaburi. Basi, akaenda mbio hadi kwa Petro na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na wala hatujui walikomweka.” Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine wakaenda kaburini. Wote wawili walikimbia lakini yule mwanafunzi mwingine alikimbia mbio kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. Alipoinama na kuchungulia ndani, aliona sanda, lakini hakuingia ndani. Simoni Petro naye akaja akimfuata, akaingia kaburini; humo akaona sanda, na kile kitambaa alichofungwa Yesu kichwani. Hicho kitambaa hakikuwekwa pamoja na hiyo sanda, bali kilikuwa kimekunjwa na kuwekwa mahali peke yake. Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyetangulia kufika kaburini, akaingia pia ndani, akaona, akaamini. ( Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko Matakatifu yaliyosema kwamba ilikuwa lazima afufuke kutoka kwa wafu). Basi, hao wanafunzi wakarudi nyumbani. Maria alikuwa amesimama nje ya kaburi, akilia. Huku akiwa bado analia, aliinama na kuchungulia kaburini, akawaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja kichwani na wa pili miguuni. Hao malaika wakamwuliza, “Mama, kwa nini unalia?” Naye akawaambia, “Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!” Baada ya kusema hayo, aligeuka nyuma, akamwona Yesu amesimama hapo, lakini asitambue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwuliza, “Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?” Maria, akidhani kwamba huyo ni mtunza bustani, akamwambia, “Mheshimiwa, kama ni wewe umemwondoa, niambie ulikomweka, nami nitamchukua.” Yesu akamwambia, “Maria!” Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, “Raboni” (yaani “Mwalimu”). Yesu akamwambia, “Usinishike; sijaenda bado juu kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu uwaambie: Naenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na Mungu wenu.” Hivyo Maria Magdalene akaenda akawapasha habari wale wanafunzi kuwa amemwona Bwana, na kwamba alikuwa amemwambia hivyo. Ilikuwa jioni ya siku hiyo ya Jumapili. Wanafunzi walikuwa wamekutana pamoja ndani ya nyumba, na milango ilikuwa imefungwa kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Basi, Yesu akaja, akasimama kati yao, akawaambia, “Amani kwenu!” Alipokwisha sema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi, hao wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana. Yesu akawaambia tena, “Amani kwenu! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma nyinyi.” Alipokwisha sema hayo, akawapulizia na kuwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa; msipowasamehe, hawasamehewi.” Thoma, mmoja wa wale kumi na wawili (aitwaye Pacha), hakuwa pamoja nao wakati Yesu alipokuja. Basi, wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.” Thoma akawaambia, “Nisipoona mikononi mwake alama za misumari na kutia kidole changu katika kovu hizo, na kutia mkono wangu ubavuni mwake, sitasadiki.” Basi, baada ya siku nane hao wanafunzi walikuwa tena pamoja mle ndani, na Thoma alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja, akasimama kati yao, akasema, “Amani kwenu!” Kisha akamwambia Thoma, “Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete mkono wako ukautie ubavuni mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini!” Thoma akamjibu, “Bwana wangu na Mungu wangu!” Yesu akamwambia, “Je, unaamini kwa kuwa umeniona? Heri yao wale ambao hawajaona, lakini wameamini.” Yesu alifanya mbele ya wanafunzi wake ishara nyingine nyingi ambazo hazikuandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mpate kuwa na uhai kwa nguvu ya jina lake. Baada ya hayo, Yesu aliwatokea tena wanafunzi wake kando ya ziwa Tiberia. Aliwatokea hivi: Simoni Petro, Thoma (aitwaye Pacha), na Nathanaeli mwenyeji wa Kana Galilaya, wana wawili wa Zebedayo na wanafunzi wake wengine wawili, walikuwa wote pamoja. Simoni Petro aliwaambia, “Nakwenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Nasi tutafuatana nawe.” Basi, wakaenda, wakapanda mashua, lakini usiku huo hawakupata chochote. Kulipoanza kupambazuka, Yesu alisimama kando ya ziwa, lakini wanafunzi hawakujua kwamba alikuwa ni yeye. Basi, Yesu akawauliza, “Vijana, hamjapata samaki wowote sio?” Wao wakamjibu, “La! Hatujapata kitu.” Yesu akawaambia, “Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua nanyi mtapata samaki.” Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza kuuvuta tena kwa wingi wa samaki. Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa), akarukia majini. Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua huku wanauvuta wavu uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa yapata mita mia kutoka ukingoni. Walipofika nchi kavu waliona moto wa makaa umewashwa na juu yake pamewekwa samaki na mkate. Yesu akawaambia, “Leteni hapa baadhi ya samaki mliovua.” Basi, Simoni Petro akapanda mashuani, akavuta hadi nchi kavu ule wavu uliokuwa umejaa samaki wakubwa 153. Na ingawa walikuwa wengi hivyo, wavu haukukatika. Yesu akawaambia, “Njoni mkafungue kinywa.” Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza: “Wewe ni nani?” maana walijua alikuwa Bwana. Yesu akaja, akatwaa mkate, akawapa; akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kutoka wafu. Walipokwisha kula, Yesu alimwuliza Simoni Petro, “Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi kuliko hawa?” Naye akajibu, “Naam, Bwana; wajua kwamba mimi nakupenda.” Yesu akamwambia, “Tunza wanakondoo wangu.” Kisha akamwambia mara ya pili, “Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?” Petro akamjibu, “Naam, Bwana; wajua kwamba nakupenda.” Yesu akamwambia, “Tunza kondoo wangu.” Akamwuliza mara ya tatu, “Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?” Hapo Petro akahuzunika kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: “Wanipenda?” Akamwambia, “Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi nakupenda.” Yesu akamwambia, “Tunza kondoo wangu! Kweli nakuambia, ulipokuwa kijana ulizoea kujifunga mshipi na kwenda kokote ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako, na mtu mwingine atakufunga na kukupeleka usikopenda kwenda.” (Kwa kusema hivyo, alionesha jinsi Petro atakavyokufa na kumtukuza Mungu). Kisha akamwambia, “Nifuate.” Hapo Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda, anafuata (Huyu mwanafunzi ndiye yule ambaye wakati wa chakula cha jioni, alikaa karibu sana na Yesu na kumwuliza: “Bwana ni nani atakayekusaliti?”) Basi, Petro alipomwona huyo, akamwuliza Yesu, “Bwana, na huyu je?” Yesu akamjibu, “Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini? Wewe nifuate mimi.” Basi, habari hiyo ikaenea miongoni mwa wale ndugu kwamba mwanafunzi huyo hafi. Lakini Yesu hakumwambia kwamba mwanafunzi huyo hafi, ila, “Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini?” Huyo ndiye yule aliyeshuhudia mambo haya na kuyaandika. Nasi twajua kwamba aliyoyasema ni kweli. Kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo kama yangeandikwa yote, moja baada ya lingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa. Ndugu Theofilo, Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. Kwa muda wa siku arubaini baada ya kifo chake aliwatokea mara nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai. Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu. Wakati alipokutana pamoja nao aliwaamuru hivi: “Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeni ile zawadi aliyoahidi Baba, ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake. Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, nyinyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.” Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, “Je, Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?” Lakini Yesu akawaambia, “Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini. Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni nyinyi, mtapokea nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia.” Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena. Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao, wakasema, “Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mlivyomwona akienda mbinguni.” Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka ule mlima uitwao Mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini. Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake. Siku moja baadaye, Petro alisimama kati ya wale ndugu waumini ambao walikuwa wamekusanyika, wote jumla watu 120, akasema, “Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni. Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu, maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu.” ( Yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu, akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje. Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba “Akel Dama,” maana yake, “Shamba la Damu.”) “Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi: ‘Makao yake yabaki mahame; mtu yeyote asiishi ndani yake.’ Tena imeandikwa: ‘Mtu mwingine achukue nafasi yake ya huduma.’ Basi, mtu mmoja miongoni mwa wale walioandamana nasi muda wote Bwana Yesu alipokuwa anasafiri pamoja nasi achaguliwe kujiunga nasi. Huyo anapaswa kuwa mmoja wa wale walioandamana nasi tangu Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni. Huyo atashiriki pamoja nasi jukumu la kushuhudia ufufuo wake Yesu.” Hapo, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia. Kisha wakasali: “Bwana, wewe unaijua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuoneshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe.” Wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja. Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika mahali pamoja. Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikaijaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa. Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha. Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani. Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Walistaajabu na kushangaa wakisema, “Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya? Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe? Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelamu; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia, Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libia karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma, Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu.” Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, “Hii ina maana gani?” Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, “Watu hawa wamelewa divai mpya!” Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu. Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi? Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli: ‘Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu wa kiume na wa kike watatoa unabii, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Naam, hata watumishi wangu wa kiume na kike, nitawamiminia Roho wangu siku zile, nao watatoa unabii. Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito; jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana. Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.’ “Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua. Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge. Maana Daudi alisema juu yake hivi: ‘Nilimwona Bwana mbele yangu daima; yuko nami upande wangu wa kulia hata sitatikisika. Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi; tena nilipiga vigelegele vya furaha. Mwili wangu utakaa katika tumaini, maana hutaiacha roho yangu kuzimu, wala kumruhusu mtakatifu wako aoze. Umenionesha njia za uhai, umenijaza furaha kwa kuwako kwako!’ “Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake liko papa hapa petu mpaka leo. Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake. Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: ‘Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza.’ Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo. Yesu alipokwisha pandishwa na kuwekwa na Mungu upande wake wa kulia, akapokea kutoka kwake Baba yule Roho Mtakatifu ambaye alituahidi, ametumiminia huyo Roho. Hicho ndicho mnachoona sasa na kusikia. Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema: ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, hadi niwafanye adui zako kiti cha miguu yako.’ “Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Kristo.” Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: “Ndugu zetu, tufanye nini?” Petro akajibu, “Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile ahadi ya Roho Mtakatifu. Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake.” Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu akisema, “Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu.” Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao 3,000 wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo. Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kindugu, kumega mkate na kusali. Miujiza na maajabu mengi yalifanyika kwa njia ya mitume hata kila mtu akajawa na hofu. Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawiana. Walikuwa wakiuza mali na vitu vyao kisha wakagawana fedha kadiri ya mahitaji ya kila mmoja. Waliendelea kukutana pamoja kila siku hekaluni. Lakini wakati wa kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula hicho kwa furaha na moyo mkunjufu. Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa. Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wakienda hekaluni, wakati wa sala. Wakati huo watu walikuwa wanambeba mtu mmoja kiwete tangu kuzaliwa. Watu hao walikuwa wakimweka huyo mtu kila siku kwenye mlango wa hekalu uitwao “Mlango Mzuri,” ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia hekaluni. Alipowaona Petro na Yohane wakiingia hekaluni, aliwaomba wampe chochote. Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, “Tutazame!” Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. Kisha Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu. Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu. Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu. Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule “Mlango Mzuri” wa hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata. Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa, wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa “Ukumbi wa Solomoni,” ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane. Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, “Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea? Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa babu zetu amemtukuza mtumishi wake Yesu. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru. Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini nyinyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe. Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uhai. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo. Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote. “Sasa ndugu zangu, mnafahamu kwamba nyinyi na wakuu wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutokujua kwenu. Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke. Basi, tubuni, mkamrudie Mungu ili yeye afute dhambi zenu. Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu. Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake watakatifu wa tangu zamani. Kwa maana Mose alisema, ‘Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii kama mimi kutoka kati yenu nyinyi wenyewe. Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa mbali na watu wa Mungu na kuangamizwa.’ Manabii wote, kuanzia Samueli na wale waliomfuata, walitangaza habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi. Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa ajili yenu; na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama alivyomwambia Abrahamu: ‘Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia zitabarikiwa.’ Basi, Mungu alimfufua mtumishi wake kwa faida yenu kwanza, akamtuma awaleteeni baraka kwa kumfanya kila mmoja wenu aachane kabisa na maovu yake.” Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa hekalu pamoja na Masadukayo walifika. Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonesha wazi kwamba wafu watafufuka. Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake. Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu wanaume 5,000. Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na waalimu wa sheria walikusanyika pamoja huko Yerusalemu. Walikutana pamoja na Anasi kuhani mkuu, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa kuhani mkuu. Walipowasimamisha mitume mbele yao, waliwauliza, “Nyinyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?” Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, “Viongozi na wazee wa watu! Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima, basi, nyinyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye nyinyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: ‘Jiwe mlilokataa nyinyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.’ Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.” Hao wazee wa Baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu. Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu. Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha. Wakaulizana, “Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba muujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo. Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu.” Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu. Lakini Petro na Yohane wakawajibu, “Amueni nyinyi wenyewe kama ni sawa mbele ya Mungu kuwatii nyinyi kuliko kumtii Mungu. Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia.” Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo. Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arubaini. Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee. Nao waliposikia habari hizo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, “Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo! Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, baba yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: ‘Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure? Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, dhidi ya Bwana na dhidi ya Kristo wake.’ “Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye ulimweka wakfu. Naam, walikutana ili wafanye mambo yale uliyokusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako. Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari. Nyosha mkono wako ili uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu.” Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila woga. Jumuiya yote ya waumini ilikuwa na moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake. Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake, “Mtu mwenye kutia moyo”). Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume. Mtu mmoja aitwaye Anania na mkewe Safira waliuza shamba lao vilevile. Lakini, mkewe akiwa anajua, Anania akajiwekea sehemu ya fedha alizopata na ile sehemu nyingine akawakabidhi mitume. Basi, Petro akamwuliza, “Anania, mbona Shetani ameuingia moyo wako na kukufanya umdanganye Roho Mtakatifu kwa kujiwekea sehemu ya fedha ulizopata kutokana na lile shamba? Kabla ya kuliuza lilikuwa mali yako, na baada ya kuliuza, bado hizo fedha zilikuwa zako uzitumie utakavyo. Kwa nini basi, uliamua moyoni mwako kufanya jambo la namna hii? Hukumdanganya mtu; umemdanganya Mungu!” Anania aliposikia hayo, akaanguka chini, akafa. Watu wote waliosikia habari za tukio hilo waliogopa sana. Vijana wakafika, wakaufunika mwili wake, wakamtoa nje, wakamzika. Baada ya muda wa saa tatu hivi, mke wake, bila kufahamu mambo yaliyotukia, akaingia mle ndani. Petro akamwambia, “Niambie! Je, kiasi hiki cha fedha ndicho mlichopata kwa kuuza lile shamba?” Yeye akamjibu, “Naam, ni kiasi hicho.” Naye Petro akamwambia, “Mbona mmekula njama kumjaribu Roho wa Bwana? Sikiliza! Wale watu waliokwenda kumzika mume wako, sasa wako mlangoni na watakuchukua wewe pia.” Mara Safira akaanguka mbele ya miguu ya Petro, akafa. Wale vijana walipoingia, walimkuta amekwisha kufa; hivyo wakamtoa nje, wakamzika karibu na mume wake. Hofu kubwa ikalikumba kanisa lote na wote waliosikia habari za tukio hilo. Mitume walifanya miujiza na maajabu mengi kati ya watu. Waumini walikuwa wakikutana pamoja katika ukumbi wa Solomoni. Mtu yeyote mwingine ambaye hakuwa mwaamini hakuthubutu kujiunga nao. Hata hivyo, watu wengine wasiokuwa wa imani hiyo waliwasifu. Idadi ya watu waliomwamini Bwana, wanaume kwa wanawake, iliongezeka zaidi na zaidi. Hata watu walikuwa wakipeleka wagonjwa barabarani na kuwalaza juu ya vitanda na mikeka ili Petro akipita, walau kivuli chake kiwaguse baadhi yao. Watu wengi walifika kutoka katika miji ya kandokando ya Yerusalemu, wakiwaleta wagonjwa wao na wale waliokuwa na pepo wachafu, nao wote wakaponywa. Kisha, kuhani mkuu na wenzake waliokuwa wa kikundi cha Masadukayo wa mahali hapo, wakawaonea mitume wivu. Basi, wakawatia nguvuni, wakawafunga ndani ya gereza kuu. Lakini usiku malaika wa Bwana aliifungua milango ya gereza, akawatoa nje, akawaambia, “Nendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uhai huu.” Mitume walitii, wakaingia hekaluni asubuhi na mapema, wakaanza kufundisha. Kuhani mkuu na wenzake walipofika, waliita mkutano wa Baraza kuu na halmashauri yote ya wazee wa Wayahudi, halafu wakawatuma watu gerezani wawalete wale mitume. Lakini hao watumishi walipofika huko hawakuwakuta mle gerezani. Hivyo walirudi, wakatoa taarifa mkutanoni, wakisema, “Tulikuta gereza limefungwa kila upande na walinzi wakilinda milango. Lakini tulipofungua hatukumkuta mtu yeyote ndani.” Mkuu wa walinzi wa hekalu na makuhani wakuu waliposikia habari hiyo wakawa na wasiwasi, wasijue yaliyowapata. Akafika mtu mmoja, akawaambia, “Wale watu mliowafunga gerezani, hivi sasa wamo hekaluni, wanawafundisha watu.” Hapo mkuu wa walinzi wa hekalu pamoja na watu wake walikwenda hekaluni, akawaleta. Lakini hawakuwakamata kwa nguvu, maana waliogopa kwamba watu wangewapiga mawe. Basi, wakawapeleka, wakawasimamisha mbele ya Baraza. Kuhani mkuu akawaambia, “Tuliwakatazeni waziwazi kufundisha kwa jina la mtu huyu; sasa mmeyaeneza mafundisho yenu pote katika Yerusalemu na mnakusudia kutuwekea lawama ya kifo cha mtu huyo.” Hapo Petro, akiwa pamoja na wale mitume wengine, akajibu, “Lazima tumtii Mungu, na siyo binadamu. Mungu wa babu zetu alimfufua Yesu baada ya nyinyi kumuua kwa kumtundika msalabani. Huyu ndiye yule aliyekwezwa na Mungu mpaka upande wake wa kulia, akawa kiongozi na Mwokozi, ili awawezeshe watu wa Israeli watubu, wapate kusamehewa dhambi zao. Sisi ni mashahidi wa tukio hilo, naye Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii, anashuhudia pia tukio hilo.” Wajumbe wote wa lile Baraza waliposikia hayo, wakawaka hasira, hata wakaamua kuwaua. Lakini Mfarisayo mmoja aitwaye Gamalieli ambaye alikuwa mwalimu wa sheria na aliyeheshimika sana mbele ya watu wote, alisimama mbele ya lile Baraza, akataka wale mitume watolewe nje kwa muda mfupi. Kisha akawaambia wale wajumbe wa Baraza, “Wananchi wa Israeli, tahadhari kabla ya kutekeleza hicho mnachotaka kuwatenda watu hawa! Zamani kidogo, kulitokea mtu mmoja jina lake Theuda, akajisema kuwa mtu wa maana na watu karibu 400 wakajiunga naye. Lakini aliuawa, kisha wafuasi wake wote wakatawanyika na kikundi chake kikafa. Tena, baadaye, wakati ule wa kuhesabiwa watu, alitokea Yuda wa Galilaya. Huyu naye aliwavuta watu wakamfuata; lakini naye pia aliuawa, na wafuasi wake wakatawanyika. Na sasa pia mimi nawaambieni, msiwachukulie watu hawa hatua yoyote; waacheni! Kwa maana, ikiwa mpango huu au shughuli yao hii imeanzishwa na binadamu, itatoweka yenyewe. Lakini kama imeanzishwa na Mungu, siyo tu kwamba hamtaweza kuwashinda, bali mtajikuta mnampinga Mungu.” Basi, wakakubaliana naye. Hivyo wakawaita wale mitume, wakaamuru wachapwe viboko na kuwaonya wasifundishe tena kwa jina la Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Basi, mitume wakatoka nje ya lile Baraza wakiwa wamejaa furaha, kwani walistahili kuaibishwa kwa ajili ya jina la Yesu. Wakaendelea kila siku kufundisha na kuhubiri Habari Njema ya Kristo hekaluni na nyumbani kwa watu. Baadaye, idadi ya wanafunzi ilipokuwa inazidi kuongezeka, kulitokea manunguniko kati ya waumini walioongea Kigiriki na wale walioongea Kiebrania. Wale walioongea Kigiriki walinungunika kwamba wajane wao walikuwa wanasahauliwa katika ugawaji wa mahitaji ya kila siku. Kwa hiyo, mitume kumi na wawili waliita jumuiya yote ya wanafunzi, wakasema, “Si vizuri sisi tuache kulihubiri neno la Mungu ili tushughulikie ugawaji wa mahitaji. Hivyo, ndugu zetu, chagueni miongoni mwenu watu saba wenye sifa njema, waliojawa na Roho na wenye hekima; nasi tutawakabidhi jukumu hilo. Sisi, lakini, tutashughulika na sala na kazi ya kuhubiri neno la Mungu.” Jambo hilo likaipendeza jumuiya yote ya waumini. Wakawachagua Stefano, mtu mwenye imani kubwa na mwenye kujaa Roho Mtakatifu, Filipo, Prokoro, Nikanori, Timona, Parmena na Nikolao wa Antiokia ambaye wakati mmoja alikuwa ameongokea dini ya Kiyahudi. Wakawaweka mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono. Neno la Mungu likazidi kuenea na idadi ya waumini huko Yerusalemu ikaongezeka zaidi, na kundi kubwa la makuhani wakaipokea imani. Mungu alimjalia Stefano neema tele, akampa nguvu nyingi hata akawa anatenda miujiza na maajabu kati ya watu. Lakini watu fulani wakatokea ili wabishane na Stefano. Baadhi ya watu hao walikuwa wa sunagogi moja lililoitwa “Sunagogi la Watu Huru”, nao walitoka Kurene na Aleksandria; wengine walitoka Kilikia na Asia. Lakini hawakuweza kumshinda kwa sababu ya hekima yake na kwa sababu ya yule Roho aliyemwongoza wakati aliposema. Kwa hiyo waliwahonga watu kadhaa waseme: “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kumkashifu Mose na kumkashifu Mungu.” Kwa namna hiyo, waliwachochea watu, wazee na waalimu wa sheria. Basi, wakamjia Stefano, wakamkamata na kumleta mbele ya Baraza Kuu. Walileta Barazani mashahidi wa uongo ambao walisema, “Mtu huyu haachi kamwe kusema maneno ya kupakashifu mahali hapa patakatifu na sheria ya Mose. Kwa maana tulikwisha msikia akisema eti huyo Yesu wa Nazareti atapaharibu kabisa mahali hapa na kufutilia mbali desturi zile tulizopokea kutoka kwa Mose.” Wote waliokuwa katika kile kikao cha Baraza walimkodolea macho Stefano, wakauona uso wake umekuwa kama wa malaika. Basi, kuhani mkuu akamwuliza, “Je, mambo haya ni kweli?” Naye Stefano akasema, “Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni! Mungu alimtokea babu yetu Abrahamu alipokuwa kule Mesopotamia kabla hajaenda kukaa kule Harani. Mungu alimwambia: ‘Ondoka katika nchi yako; waache watu wa ukoo wako; nenda katika nchi nitakayokuonesha!’ Kwa hivyo, Abrahamu alihama nchi ya Kaldayo, akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu alimtoa tena Harani akaja kukaa katika nchi hii mnayokaa sasa. Mungu hakumpa hata sehemu moja ya nchi hii iwe mali yake; hata hivyo, alimwahidi kumpa nchi hii iwe yake na ya wazawa wake, ingawaje wakati huu hakuwa na mtoto. Mungu alimwambia hivi: ‘Wazawa wako watapelekwa katika nchi inayotawaliwa na watu wengine, na huko watafanywa watumwa na kutendewa vibaya kwa muda wa miaka 400. Lakini mimi nitalihukumu taifa hilo litakalowafanya watumwa. Kisha nitawatoa katika nchi hiyo ili waje kuniabudu mahali hapa.’ Halafu Mungu akafanya naye agano ambalo tohara ni ishara yake. Hivyo, Abrahamu alimtahiri mtoto wake Isaka siku ya nane baada ya kuzaliwa. Na Isaka, vivyo hivyo, alimtahiri Yakobo. Naye Yakobo aliwatendea wale mababu kumi na wawili vivyo hivyo. “Wale mababu walimwonea wivu Yosefu, wakamwuza utumwani Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, akamwokoa katika taabu zake zote. Mungu alimjalia fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri, hata Farao akamweka awe mkuu wa ile nchi na nyumba ya kifalme. Kisha, kulizuka njaa kubwa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa. Babu zetu hawakuweza kupata chakula chochote. Basi, Yakobo aliposikia habari kwamba huko Misri kulikuwa na nafaka, aliwatuma watoto wake, yaani babu zetu, waende huko Misri mara ya kwanza. Katika safari yao ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, na Farao akaifahamu jamaa ya Yosefu. Yosefu alituma ujumbe kwa baba yake na jamaa yote, jumla watu sabini na watano, waje Misri. Hivyo, Yakobo alikwenda Misri ambako yeye na babu zetu wengine walikufa. Miili yao ililetwa mpaka Shekemu, ikazikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alikuwa amenunua kutoka kwa kabila la Hamori kwa kiasi fulani cha fedha. “Wakati ulipotimia Mungu aitimize ahadi aliyompa Abrahamu, idadi ya wale watu kule Misri ilikwisha ongezeka na kuwa kubwa zaidi. Mwishowe, mfalme mmoja ambaye hakumtambua Yosefu alianza kutawala huko Misri. Alilifanyia taifa letu ukatili, akawatendea vibaya babu zetu kwa kuwalazimisha waweke nje watoto wao wachanga ili wafe. Mose alizaliwa wakati huo. Alikuwa mtoto mzuri sana. Alilelewa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu, na alipotolewa nje, binti wa Farao alimchukua, akamlea kama mtoto wake. Mose alifundishwa mambo yote ya hekima ya Wamisri akawa mashuhuri kwa maneno na matendo. “Alipokuwa na umri wa miaka arubaini aliamua kwenda kuwaona ndugu zake Waisraeli. Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda kumwokoa, na kwa kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri. ( Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo). Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha akisema: ‘Nyinyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya nyinyi kwa nyinyi?’ Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’ Baada ya kusikia hayo, Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili. “Miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana alimtokea Mose katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na mlima Sinai. Mose alistaajabu sana kuona tukio hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana: ‘Mimi ni Mungu wa babu zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo!’ Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi. Bwana akamwambia: ‘Vua viatu vyako maana hapa unaposimama ni mahali patakatifu. Nimeyaona mabaya wanayotendewa watu wangu kule Misri. Nimesikia kilio chao, nami nimekuja kuwaokoa. Basi sasa, nitakutuma Misri.’ “Huyu Mose ndiye yule watu wa Israeli waliyemkataa waliposema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?’ Kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu alimtuma Mose huyo awe kiongozi na mkombozi. Ndiye aliyewaongoza wale watu watoke Misri kwa kufanya miujiza na maajabu katika nchi ya Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani, kwa muda wa miaka arubaini. Mose ndiye aliyewaambia watu wa Israeli: ‘Mungu atawateulieni nabii kama mimi miongoni mwa ndugu zenu nyinyi wenyewe.’ Waisraeli walipokusanyika kule jangwani, Mose ndiye aliyekuwako huko kama mjumbe kati ya hao wazee wetu na yule malaika aliyeongea naye mlimani Sinai. Ndiye aliyekabidhiwa yale maneno ya uhai atupe sisi. “Lakini yeye ndiye babu zetu waliyekataa kumsikiliza; walimsukuma kando, wakatamani kurudi Misri. Walimwambia Aroni: ‘Tutengenezee miungu itakayotuongoza njiani, maana hatujui yaliyompata huyo Mose aliyetuongoza kutoka Misri!’ Hapo ndipo walipojitengenezea sanamu ya ndama, wakaitambikia na kukifanyia sherehe kitu ambacho ni kazi ya mikono yao wenyewe. Lakini Mungu aliondoka kati yao, akawaacha waabudu nyota za anga, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii: ‘Enyi watu wa Israeli! Si mimi mliyenitolea tambiko na sadaka kwa miaka arubaini kule jangwani! Nyinyi mlikibeba kibanda cha mungu Moloki, na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani. Sanamu mlizozifanya ndizo mlizoabudu. Kwa sababu hiyo nitawapeleka mateka mbali kupita Babuloni!’ Kule jangwani babu zetu walikuwa na lile hema la maamuzi. Lilitengenezwa kama Mungu alivyomwambia Mose alifanye; nakala kamili ya kile alichooneshwa. Kisha babu zetu walilipokezana wao kwa wao mpaka wakati wa Yoshua, walipoinyakua ile nchi kutoka kwa mataifa ambayo Mungu aliyafukuza mbele yao. Hapo lilikaa mpaka nyakati za Daudi. Daudi alipata upendeleo kwa Mungu, akamwomba Mungu ruhusa ya kumjengea makao yeye aliye Mungu wa Yakobo. Lakini Solomoni ndiye aliyemjengea Mungu nyumba. “Hata hivyo, Mungu Mkuu haishi katika nyumba zilizojengwa na binadamu; kama nabii asemavyo: ‘Bwana asema: Mbingu ni kiti changu cha enzi na dunia ni kiti changu cha kuwekea miguu. Ni nyumba ya namna gani basi mnayoweza kunijengea, na ni mahali gani nitakapopumzika? Vitu hivi vyote ni mimi nimevifanya, au sivyo?’ “Enyi wakaidi wakuu! Mioyo na masikio yenu ni kama ya watu wa mataifa. Nyinyi ni kama babu zenu. Siku zote mnampinga Roho Mtakatifu. Je, yuko nabii yeyote ambaye babu zenu hawakumtesa? Waliwaua hao Mungu aliowatuma watangaze kuja kwake yule Mwenye Haki. Na sasa, nyinyi mmemsaliti, mkamuua. Nyinyi mliipokea ile sheria iliyoletwa kwenu na Malaika, lakini hamkuitii.” Wale wazee wa Baraza waliposikia hayo, walighadhibika sana, wakamsagia meno kwa hasira. Lakini Stefano akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akatazama juu mbinguni, akauona utukufu wa Mungu na Yesu amekaa upande wa kulia wa Mungu. Akasema, “Tazameni! Ninaona mbingu zimefunuliwa na Mwana wa Mtu amesimama upande wa kulia wa Mungu.” Hapo, watu wote katika kile kikao cha Baraza, wakapiga kelele na kuziba masikio yao kwa mikono yao. Kisha wakamrukia wote kwa pamoja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga mawe. Wale mashahidi wakayaweka makoti yao chini ya ulinzi wa kijana mmoja jina lake Saulo. Waliendelea kumpiga Stefano kwa mawe huku akiwa anasali: “Bwana Yesu, ipokee roho yangu!” Akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa: “Bwana, usiwalaumu kwa sababu ya dhambi hii.” Baada ya kusema hivyo, akafa. Saulo naye alikiona kitendo hicho cha kumwua kuwa sawa. Siku hiyo kanisa la Yerusalemu lilianza kuteswa vibaya. Waumini wote, isipokuwa tu wale mitume, walilazimika kutawanyika katika sehemu za mashambani za Yudea na Samaria. Watu wamchao Mungu walimzika Stefano na kumfanyia maombolezo makubwa. Wakati huohuo, Saulo alijaribu kuliangamiza kanisa. Alikwenda katika kila nyumba, akawatoa nje waumini, wanaume kwa wanawake, akawatia gerezani. Wale waumini waliotawanyika, walikwenda kila mahali wakihubiri ule ujumbe. Naye Filipo aliingia katika mji wa Samaria na kumhubiri Kristo kwa wenyeji wa hapo. Watu walijiunga kusikiliza kwa makini ule ujumbe wa Filipo na kuona ile miujiza aliyoifanya. Maana pepo wachafu waliokuwa wamewapagaa watu wengi waliwatoka wakipiga kelele kubwa; na pia watu wengi waliokuwa wamepooza viungo na waliolemaa waliponywa. Kukawa na furaha kubwa katika mji ule. Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Simoni ambaye alikuwa amekwisha fanya uchawi wake katika mji huo kwa muda na kuwashangaza watu wa Samaria, akijiona kuwa yeye ni mtu maarufu. Watu wote, wadogo kwa wakubwa, walimsikiliza kwa makini wakisema, “Simoni ndiye nguvu ya kimungu inayoitwa ‘Nguvu Kubwa.’” Walivutiwa sana naye kwa vile alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake kwa muda mrefu. Lakini walipouamini ujumbe wa Filipo juu ya Habari Njema ya ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, walibatizwa, wanawake na wanaume. Hata Simoni aliamini; na baada ya kubatizwa alikuwa akiandamana na Filipo, akastaajabia maajabu na miujiza iliyokuwa inafanyika. Wale mitume waliokuwa kule Yerusalemu walipopata habari kwamba wenyeji wa Samaria nao wamelipokea neno la Mungu, waliwatuma huko Petro na Yohane. Walipofika waliwaombea hao waumini ili wampokee Roho Mtakatifu; maana wakati huo Roho Mtakatifu hakuwa amemshukia yeyote kati yao; walikuwa wamebatizwa tu kwa jina la Bwana Yesu. Basi, Petro na Yohane wakawawekea mikono hao waumini, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hapo Simoni alingamua kwamba kwa kuwekewa mikono ya mitume waumini walipewa Roho Mtakatifu. Hivyo aliwapa Petro na Yohane fedha akisema, “Nipeni na mimi uwezo huo ili yeyote nitakayemwekea mikono, apokee Roho Mtakatifu.” Lakini Petro akamjibu, “Potelea mbali na fedha zako kwa vile unafikiri kwamba unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha! Huna sehemu yoyote wala haki katika kazi hiyo kwa maana moyo wako hauko sawa mbele ya macho ya Mungu. Kwa hiyo, tubu ubaya wako huu na umwombe Bwana naye anaweza kukusamehe fikira kama hizo. Ni dhahiri kwangu kwamba umejaa wivu mkali na u mfungwa wa dhambi!” Simoni akajibu, “Tafadhali, niombeeni kwa Bwana lisije likanipata lolote kati ya hayo mliyosema.” Baada ya Petro na Yohane kutoa ushuhuda wao na kuutangaza ujumbe wa Bwana, walirudi Yerusalemu. Walipokuwa wanarudi walihubiri Habari Njema katika vijiji vingi vya Samaria. Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jitayarishe uende kusini kupitia njia inayotoka Yerusalemu kwenda Gaza.” (Njia hiyo hupita jangwani). Basi, Filipo akajiweka tayari, akaanza safari. Wakati huohuo kulikuwa na Mwethiopia mmoja, towashi, ambaye alikuwa anasafiri kuelekea nyumbani. Huyo mtu alikuwa mkurugenzi maarufu wa hazina ya Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa amekwenda huko Yerusalemu kuabudu na wakati huo alikuwa anarudi akiwa amepanda gari la kukokotwa. Alipokuwa anasafiri, alikuwa akijisomea kitabu cha nabii Isaya. Basi, Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda karibu na gari hilo ukafuatane nalo.” Filipo akakimbilia karibu na gari, akamsikia huyo mtu akisoma katika kitabu cha nabii Isaya. Hapo Filipo akamwuliza, “Je, unaelewa hayo unayosoma?” Huyo mtu akamjibu, “Ninawezaje kuelewa bila mtu kuniongoza?” Hapo akamwalika Filipo apande juu, aketi pamoja naye. Basi, sehemu ya Maandiko Matakatifu aliyokuwa anasoma ilikuwa hii: “Alikuwa kama kondoo anayepelekwa kuchinjwa; kimya kama vile mwanakondoo anapokatwa manyoya, yeye hakutoa sauti hata kidogo. Alifedheheshwa na kunyimwa haki. Hakuna atakayeweza kuongea juu ya kizazi chake, kwa maana maisha yake yameondolewa duniani.” Huyo Mwethiopia akamwambia Filipo, “Niambie, huyu nabii anasema juu ya nini? Anasema mambo haya juu yake yeye mwenyewe au juu ya mtu mwingine?” Basi, Filipo akianzia na sehemu hiyo ya Maandiko Matakatifu, akamweleza Habari Njema juu ya Yesu. Walipokuwa bado wanaendelea na safari, walifika mahali penye maji, na huyo ofisa akasema, “Mahali hapa pana maji; je, kuna chochote cha kunizuia nisibatizwe?” [ Filipo akasema, “Kama unaamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa.” Naye akajibu, “Naam, ninaamini kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.”] Basi, huyo ofisa akaamuru lile gari lisimame; na wote wawili, Filipo na huyo towashi wakashuka majini, naye Filipo akambatiza. Walipotoka majini Roho wa Bwana akamfanya Filipo atoweke. Na huyo towashi hakumwona tena; lakini akaendelea na safari yake mwenye furaha. Filipo akajikuta yuko Azoto, akapita katika miji yote akihubiri Injili mpaka alipofika Kaisarea. Wakati huo Saulo alikuwa akizidisha vitisho vikali vya kuwaua wafuasi wa Bwana. Alikwenda kwa kuhani mkuu, akaomba apatiwe barua za utambulisho kwa masunagogi ya Kiyahudi kule Damasko, ili akikuta huko wanaume au wanawake wanaofuata Njia hiyo, awakamate na kuwaleta Yerusalemu. Lakini alipokuwa njiani karibu kufika Damasko, ghafla mwanga kutoka angani ulimwangazia pande zote. Akaanguka chini na kusikia sauti ikimwambia: “Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?” Naye Saulo akauliza, “Ni nani wewe Bwana?” Na ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa. Lakini simama sasa, uingie mjini na huko utaambiwa unachopaswa kufanya.” Wale watu waliokuwa wanasafiri pamoja na Saulo walisimama pale, wakiwa hawana la kusema; walisikia ile sauti lakini hawakumwona mtu. Saulo aliinuka, na alipofumbua macho yake hakuweza kuona chochote; hivyo wale watu wakamwongoza kwa kumshika mkono mpaka mjini Damasko. Saulo alikaa siku tatu bila kuona, na wakati huo hakula au kunywa chochote. Basi, huko Damasko kulikuwa na mfuasi mmoja aitwaye Anania. Bwana akamwambia katika maono, “Anania!” Anania akaitika, “Niko hapa, Bwana.” Naye Bwana akamwambia, “Jitayarishe uende kwenye barabara inayoitwa Barabara ya Moja kwa Moja, na katika nyumba ya Yuda umtake mtu mmoja kutoka Tarso aitwaye Saulo. Sasa anasali; na katika maono ameona mtu aitwaye Anania akiingia ndani na kumwekea mikono ili apate kuona tena.” Lakini Anania akajibu, “Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kutoka kwa watu wengi; nimesikia juu ya mabaya aliyowatendea watu wako huko Yerusalemu. Na amekuja hapa akiwa na mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu kuwatia nguvuni wote wanaoomba kwa jina lako.” Lakini Bwana akamwambia, “Nenda tu, kwa maana nimemchagua awe chombo changu, alitangaze jina langu kwa mataifa na wafalme wao na kwa watu wa Israeli. Mimi mwenyewe nitamwonesha mengi yatakayomlazimu kuteswa kwa ajili ya jina langu.” Basi, Anania akaenda, akaingia katika hiyo nyumba. Kisha akaweka mikono yake juu ya Saulo, akasema, “Ndugu Saulo, Bwana ambaye ndiye Yesu mwenyewe aliyekutokea ulipokuwa njiani kuja hapa, amenituma ili upate kuona tena na kujazwa Roho Mtakatifu.” Mara vitu kama magamba vikaanguka kutoka machoni mwa Saulo, akaweza kuona tena. Akasimama, akabatizwa. Na baada ya kula chakula, nguvu zake zikamrudia. Saulo alikaa siku chache pamoja na wafuasi huko Damasko. Mara alianza kuhubiri katika masunagogi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. Watu wote waliomsikia walishangaa, wakasema, “Je, mtu huyu si yuleyule aliyewaua wale waliokuwa wanaomba kwa jina hili kule Yerusalemu? Tena alikuja hapa akiwa na madhumuni ya kuwatia nguvuni watu hao na kuwapeleka kwa makuhani!” Saulo alizidi kupata nguvu, na kwa jinsi alivyothibitisha wazi kwamba Yesu ndiye Kristo, Wayahudi wa huko Damasko walivurugika kabisa. Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi walikusanyika na kufanya mpango wa kumuua Saulo. Lakini Saulo alipata habari ya mpango huo. Usiku na mchana walilinda milango ya kuingia mjini ili wapate kumuua. Lakini wakati wa usiku wanafunzi wake walimchukua, wakamteremsha chini ndani ya kapu kubwa kwa kupitia nafasi iliyokuwako ukutani. Saulo alipofika Yerusalemu alijaribu kujiunga na wale wanafunzi. Lakini wote walimwogopa hawakuweza kuamini kwamba yeye amekuwa mfuasi. Hapo, Barnaba alikuja akamchukua Saulo, akampeleka kwa mitume na kuwaeleza jinsi Saulo alivyomwona Bwana njiani na jinsi Bwana alivyoongea naye. Aliwaambia pia jinsi Saulo alivyokuwa amehubiri bila woga kule Damasko. Basi, Saulo alikaa pamoja nao, akatembelea Yerusalemu yote akihubiri neno la Bwana bila hofu. Pia aliongea na kubishana na Wayahudi wanaoongea Kigiriki, lakini wao walijaribu kumwua. Wale ndugu walipogundua jambo hilo, walimchukua Saulo, wakampeleka Kaisarea, wakamwacha aende zake Tarso. Wakati huo kanisa likawa na amani popote katika Yudea, Galilaya, na Samaria. Lilijengwa na kukua katika kumcha Bwana, na kuongezeka likitiwa moyo na Roho Mtakatifu. Petro alipokuwa anasafirisafiri kila mahali alifika pia kwa watu wa Mungu waliokuwa wanaishi Luda. Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea ambaye kwa muda wa miaka minane alikuwa amelala kitandani kwa sababu alikuwa amepooza. Basi, Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya. Amka utandike kitanda chako.” Ainea akaamka mara. Wakazi wote wa Luda na Saroni walimwona Ainea, na wote wakamgeukia Bwana. Kulikuwa na mfuasi mmoja mwanamke mjini Yopa aitwaye Tabitha (kwa Kigiriki ni Dorka, maana yake, Paa). Huyo mwanamke alikuwa akitenda mema na kuwasaidia maskini daima. Wakati huo ikawa kwamba aliugua, akafa. Watu wakauosha mwili wake, wakaulaza katika chumba ghorofani. Yopa si mbali sana na Luda; kwa hiyo wafuasi waliposikia kwamba Petro alikuwa Luda, wakawatuma watu wawili kwake na ujumbe: “Njoo kwetu haraka iwezekanavyo.” Basi, Petro akaenda pamoja nao. Alipofika alipelekwa ghorofani katika kile chumba. Huko wajane wengi walimzunguka Petro wakilia na kumwonesha makoti na nguo ambazo Dorka alikuwa akitengeneza wakati alipokuwa hai. Petro aliwatoa nje wote, akapiga magoti, akasali. Kisha akaigeukia ile maiti, akasema, “Tabitha, amka.” Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro, akaketi. Petro akamsaidia kusimama, halafu akawaita wale watu wa Mungu na wale wajane, akamkabidhi kwao akiwa mzima. Habari za tukio hili zilienea kila mahali huko Yopa, na watu wengi wakamwamini Bwana. Petro alikaa siku kadhaa huko Yopa, akiishi kwa mtu mmoja mtengenezaji wa ngozi aitwaye Simoni. Kulikuwa na mtu mmoja huko Kaisarea aitwaye Kornelio, jemadari wa kikosi kimoja kiitwacho “Kikosi cha Italia.” Alikuwa mtu mwema; naye pamoja na jamaa yake yote walimcha Mungu; alikuwa anafanya mengi kusaidia maskini wa Kiyahudi na alikuwa anasali daima. Yapata saa tisa alasiri, aliona dhahiri katika maono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, “Kornelio!” Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, “Kuna nini Mheshimiwa?” Huyo malaika akamwambia, “Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini wala hatazisahau. Sasa, watume watu Yopa wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. Yeye yumo nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko karibu na bahari.” Huyo malaika aliyesema hayo alipokwisha kwenda zake, Kornelio aliwaita watumishi wawili wa nyumbani na mmoja wa askari zake ambaye alikuwa mcha Mungu, akawaeleza yote yaliyotukia, akawatuma Yopa. Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali. Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, akaota ndoto. Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne. Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: Wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani. Akasikia sauti ikimwambia: “Petro, amka uchinje, ule!” Petro akajibu, “La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu.” Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: “Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!” Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni. Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hayo maono aliyokuwa ameyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni, wakaita kwa sauti: “Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?” Petro alikuwa bado anajaribu kuelewa yale maono, na hapo Roho akamwambia, “Sikiliza! Kuna watu watatu hapa, wanakutafuta. Shuka upesi na wala usisite kwenda pamoja nao kwa maana ni mimi niliyewatuma.” Basi, Petro akateremka chini, akawaambia hao watu, “Mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?” Wao wakamjibu, “Jemadari Kornelio ambaye ni mtu mwema, mcha Mungu na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote, ametutuma. Aliambiwa na malaika mtakatifu akualike nyumbani kwake ili asikilize chochote ulicho nacho cha kusema.” Petro akawakaribisha ndani, akawapa mahali pa kulala usiku ule. Kesho yake, Petro alianza safari pamoja nao, na baadhi ya ndugu wa huko Yopa walifuatana naye. Siku ya pili yake walifika Kaisarea na huko Kornelio alikuwa anawangojea pamoja na jamaa na marafiki aliokuwa amewaalika. Petro alipokuwa anaingia, Kornelio alitoka nje kumlaki, akapiga magoti mbele yake na kuinama chini kabisa. Lakini Petro alimwinua, akamwambia, “Simama, kwa maana mimi ni binadamu tu.” Petro aliendelea kuongea na Kornelio wakiwa wanaingia nyumbani ambamo aliwakuta watu wengi wamekusanyika. Petro akawaambia, “Nyinyi wenyewe mnajua kwamba Myahudi yeyote amekatazwa na sheria yake ya dini kushirikiana na watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amenijulisha nisimfikirie mtu yeyote kuwa najisi au mchafu. Kwa sababu hiyo, mliponiita nimekuja bila kusita. Basi, nawaulizeni: Kwa nini mmeniita?” Kornelio akasema, “Siku tatu zilizopita saa kama hii, saa tisa alasiri, nilikuwa nikisali chumbani mwangu. Ghafla, mtu aliyekuwa amevaa mavazi yenye kungaa alisimama mbele yangu, akasema: ‘Kornelio! Sala yako na sadaka zako kwa maskini zimekubaliwa na Mungu. Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro; yuko nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi karibu na bahari.’ Kwa hiyo nilikutumia ujumbe bila kuchelewa, nawe umefanya vyema kuja. Sasa, sisi tuko mbele ya Mungu, kusikiliza chochote ambacho Bwana amekuamuru kusema.” Hapo Petro akaanza kusema: “Sasa nimetambua kwamba hakika Mungu hana ubaguzi. Mtu wa taifa lolote anayemcha Mungu na kutenda yaliyo sawa anapokelewa naye. Huu ndio ule ujumbe Mungu alioupeleka kwa watu wa Israeli, akitangaza Habari Njema iletayo amani kwa njia ya Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa wote. Nyinyi mnajua jambo lililotukia katika nchi yote ya Wayahudi kuanzia Galilaya baada ya ule ubatizo aliohubiri Yohane. Mnamjua Yesu wa Nazareti na jinsi Mungu alivyomteua kwa kummiminia Roho Mtakatifu na nguvu. Mungu alikuwa pamoja naye; yeye alikwenda huko na huko akitenda mema na kuwaponya wote waliokuwa wamevamiwa na Ibilisi. Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyotenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu. Walimuua kwa kumtundika msalabani; lakini Mungu alimfufua siku ya tatu, akamfanya aonekane, si kwa watu wote, ila kwa wale Mungu aliokwisha wachagua wawe mashahidi wake, yaani sisi tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. Alituamuru kuihubiri Habari Njema kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyeteuliwa na Mungu awe Mwamuzi wa walio hai na wafu. Manabii wote waliongea juu yake kwamba kila mtu atakayemwamini atasamehewa dhambi zake zote kwa jina lake.” Wakati Petro alipokuwa bado anasema maneno hayo, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanasikiliza ujumbe huo. Wale Wayahudi waumini waliokuja pamoja na Petro kutoka Yopa walishangaa kuona kuwa Mungu aliwamiminia kipawa cha Roho Mtakatifu watu wa mataifa mengine pia; maana waliwasikia wakiongea kwa lugha mbalimbali wakimtukuza Mungu. Hapo Petro akasema, “Watu hawa wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi wenyewe tulivyompokea. Je, kuna yeyote atakayeweza kuwazuia wasibatizwe kwa maji?” Basi, akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba akae nao kwa siku chache. Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu. Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema: “Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao! Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo: “Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa ikishushwa chini kutoka mbinguni ikiwa imeshikwa pembe zake nne, ikawekwa kando yangu. Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani. Kisha nikasikia sauti ikiniambia: ‘Petro amka, chinja, ule.’ Lakini mimi nikasema: ‘La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.’ Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: ‘Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.’ Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni. Ghafla, watu watatu waliokuwa wametumwa kwangu kutoka Kaisarea waliwasili kwenye nyumba nilimokuwa nakaa. Roho aliniambia niende pamoja nao bila kusita. Hawa ndugu sita waliandamana nami pia kwenda Kaisarea na huko tuliingia nyumbani mwa Kornelio. Yeye alitueleza jinsi alivyokuwa amemwona malaika amesimama nyumbani mwake na kumwambia: ‘Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. Yeye atakuambia maneno ambayo kwayo wewe na jamaa yako yote mtaokolewa.’ Na nilipoanza tu kuongea, Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyotushukia sisi pale awali. Hapo nilikumbuka yale maneno Bwana aliyosema: ‘Yohane alibatiza kwa maji, lakini nyinyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.’ Basi, kama Mungu amewapa pia watu wa mataifa mengine kipawa kilekile alichotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, je, mimi ni nani hata nijaribu kumpinga Mungu?” Waliposikia hayo, waliacha ubishi, wakamtukuza Mungu wakisema, “Mungu amewapa watu wa mataifa mengine nafasi ya kutubu wapate uhai!” Kutokana na mateso yaliyotokea wakati Stefano alipouawa, waumini walitawanyika. Wengine walikwenda mpaka Foinike, Kupro na Antiokia wakihubiri ule ujumbe kwa Wayahudi tu. Lakini baadhi ya waumini waliotoka Kupro na Kurene, walikwenda Antiokia wakautangaza huo ujumbe kwa watu wa mataifa mengine wakiwahubiria Habari Njema juu ya Bwana Yesu. Bwana aliwasaidia na idadi kubwa ya watu iliamini na kumgeukia Bwana. Habari ya jambo hilo ikasikika kwa lile kanisa la Yerusalemu. Hivyo wakamtuma Barnaba aende Antiokia. Alipofika huko na kuona jinsi Mungu alivyowaneemesha wale watu, alifurahi na kuwahimiza wote wadumu katika uaminifu wao kwa Bwana. Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana. Kisha, Barnaba alikwenda Tarso kumtafuta Saulo. Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na ile jumuiya ya kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo. Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu. Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote. (Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio). Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea. Basi, wakafanya hivyo na kuwapa Barnaba na Saulo mchango huo wauwasilishe wao wenyewe kwa wazee wa kanisa. Karibu wakati huohuo, mfalme Herode alianza kuwatesa baadhi ya Wakristo. Alimuua kwa upanga Yakobo, ndugu yake Yohane. Alipoona kuwa kitendo hicho kiliwapendeza Wayahudi, aliendelea, akamkamata Petro. (Hiyo ilifanyika wakati wa sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu). Baada ya kutiwa nguvuni, Petro alifungwa gerezani, akawekwa chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari wannewanne. Herode alikusudia kumtoa hadharani baada ya sikukuu ya Pasaka. Basi, Petro alipokuwa gerezani, kanisa lilikuwa linamwombea kwa Mungu kwa moyo. Usiku, kabla ya siku ile ambayo Herode angemtoa Petro hadharani, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili. Alikuwa amefungwa minyororo miwili, na walinzi walikuwa wanalinda lango la gereza. Ghafla, malaika wa Bwana akasimama karibu naye na mwanga ukaangaza kile chumba cha gereza. Malaika akamgusa ubavuni akamwamsha akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo iliyomfunga mikono ikakatika na kuanguka chini. Malaika akamwambia, “Jifunge mshipi wako, vaa viatu vyako.” Akafanya hivyo. Kisha huyo malaika akamwambia, “Vaa koti lako, unifuate.” Petro akamfuata nje lakini hakujua kama hayo yaliyofanywa na huyo malaika yalikuwa ya kweli; alidhani alikuwa anaota ndoto. Walipita kituo cha kwanza cha ulinzi na cha pili, halafu wakafika kwenye mlango wa chuma wa kuingilia mjini. Huo mlango ukawafungukia wenyewe, nao wakatoka nje. Wakawa wanatembea katika barabara moja na mara yule malaika akamwacha Petro peke yake. Hapo ndipo Petro alipotambua yaliyotukia, akasema, “Sasa najua kwa hakika kwamba Bwana amemtuma malaika wake akaniokoa mikononi mwa Herode na kutoka katika mambo yale yote watu wa Israeli waliyotazamia.” Alipotambua hivyo alikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Maria mama yake Yohane aitwaye Marko. Humo watu wengi walikuwa wamekusanyika wakisali. Petro alipiga hodi kwenye mlango wa nje na mtumishi mmoja msichana aitwaye Roda, akaenda mlangoni kuitikia. Huyo msichana aliitambua sauti ya Petro akafurahi mno, hata badala ya kuufungua ule mlango, akakimbilia ndani na kuwaambia kwamba Petro alikuwa amesimama nje mlangoni. Wakamwambia yule msichana, “Una wazimu!” Lakini yeye akasisitiza kwamba ilikuwa kweli. Nao wakamwambia, “Huyo ni malaika wake.” Wakati huo Petro alikuwa anaendelea kupiga hodi. Mwishowe walifungua mlango, wakamwona, wakashangaa. Petro aliwaashiria kwa mkono wakae kimya, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa gerezani. Kisha akawaambia watoe taarifa ya jambo hilo kwa Yakobo na wale ndugu wengine, halafu akatoka akaenda mahali pengine. Kulipokucha, ulitokea wasiwasi mkubwa kati ya wale askari kuhusu yaliyokuwa yamempata Petro. Herode aliamuru ufanywe msako lakini hawakuweza kumpata. Hivyo aliamuru wale askari wahojiwe, akatoa amri wauawe. Halafu akatoka huko Yudea, akaenda Kaisarea ambako alikaa. Herode alikasirishwa sana na watu wa Tiro na Sidoni. Lakini wao walimpelekea wajumbe. Nao wakafaulu kwanza kumpata Blasto awe upande wao. Blasto alikuwa msimamizi mkuu wa ikulu ya mfalme. Kisha, wakamwendea Herode wakamwomba kuwe na amani, kwa maana nchi yao ilitegemea nchi ya mfalme kwa chakula. Siku moja iliyochaguliwa, Herode akiwa amevaa mavazi rasmi na kuketi katika kiti cha kifalme, aliwahutubia watu. Wale watu walimpigia kelele za shangwe wakisema, “Hii ni sauti ya mungu, si ya mtu.” Papo hapo malaika wa Bwana akamwangusha Herode chini kwa sababu hakumpa Mungu hizo sifa. Akaliwa na wadudu, akafa. Neno la Mungu likazidi kuenea na kukua. Baada ya Barnaba na Saulo kutekeleza huduma yao, walitoka tena Yerusalemu, wakamchukua Yohane aitwaye pia Marko. Katika kanisa la Antiokia kulikuwa na watu wengine waliokuwa manabii na waalimu; miongoni mwao wakiwa Barnaba, Simoni aitwaye pia Mweusi, Lukio wa Kurene, Manaeni ambaye alikuwa amelelewa pamoja na mfalme Herode, na Saulo. Walipokuwa wanafanya ibada yao kwa Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema: “Niteulieni Barnaba na Saulo kwa ajili ya kazi niliyowaitia.” Basi, baada ya kusali na kufunga zaidi, wakawawekea mikono, wakawaacha waende zao. Basi, Barnaba na Saulo walipokwisha tumwa na Roho Mtakatifu, walishuka hadi Seleukia, na kutoka huko walipanda meli hadi kisiwa cha Kupro. Walipofika Salami walihubiri neno la Mungu katika masunagogi ya Kiyahudi. Yohane alikuwa msaidizi wao. Walitembea toka upande mmoja wa kisiwa mpaka Pafo, upande wa pili, na huko walimkuta mchawi mmoja Myahudi aitwaye Bar-yesu ambaye alijisingizia kuwa nabii. Huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mkuu wa kile kisiwa, ambaye alikuwa mtu mwelewa sana. Sergio Paulo aliwaita Barnaba na Saulo ili asikie neno la Mungu. Lakini huyo mchawi Elima, (kama alivyokuwa anaitwa kwa Kigiriki), alijaribu kuwapinga ili kumzuia huyo mkuu wa kisiwa asije akaigeukia imani ya Kikristo. Basi, Saulo ambaye aliitwa pia Paulo, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkodolea macho huyo mchawi, akasema, “Mdanganyifu wa kupindukia na mlaghai wewe! Wewe ni mtoto wa Ibilisi! Wewe ni adui wa chochote kile kilicho cha kweli; hukomi hata mara moja kujaribu kuzipotosha njia za Bwana zilizonyoka. Sasa, mkono wa Bwana utakuadhibu: Utakuwa kipofu na hutaweza kuuona mwanga wa jua kwa kitambo.” Mara kila kitu kikawa kama ukungu na giza kwake, akaanza kwenda huku na huko akitafuta mtu wa kumshika mkono amwongoze. Yule mkuu wa kisiwa alipoona hayo, aliongoka akawa mwaamini; akastaajabia sana mafundisho aliyosikia juu ya Bwana. Kutoka Pafo, Paulo na wenzake walipanda meli wakaenda hadi Perga katika Pamfulia; lakini Yohane aliwaacha, akarudi Yerusalemu. Lakini wao waliendelea na safari toka Perga hadi mjini Antiokia Pisidia. Siku ya Sabato waliingia ndani ya sunagogi, wakakaa. Baada ya masomo katika kitabu cha sheria ya Mose na katika maandiko ya manabii, wakuu wa lile sunagogi waliwapelekea ujumbe huu: “Ndugu, kama mnalo jambo la kuwaambia watu ili kuwapa moyo, semeni.” Basi, Paulo alisimama, akatoa ishara kwa mkono, akaanza kuongea: “Wananchi wa Israeli na wengine wote mnaomcha Mungu, sikilizeni! Mungu wa watu hawa wa Israeli aliwachagua babu zetu; aliwafanya watu hawa wawe taifa kubwa walipokuwa ugenini kule Misri. Mungu aliwatoa huko kwa uwezo wake mkuu. Aliwavumilia kwa muda wa miaka arubaini kule jangwani. Aliyaangamiza mataifa saba ya nchi ya Kanaani akawapa hao watu wake ile nchi kuwa mali yao. Miaka 450 ilipita, halafu akawapatia waamuzi wawaongoze mpaka wakati wa nabii Samueli. Hapo wakapendelea kuwa na mfalme, na Mungu akawapa Shauli, mtoto wa Kishi wa kabila la Benyamini, awe mfalme wao kwa muda wa miaka arubaini. Baada ya kumwondoa Shauli, Mungu alimteua Daudi kuwa mfalme wao. Mungu alionesha kibali chake kwake akisema: ‘Nimemwona Daudi mtoto wa Yese; ni mtu anayepatana na moyo wangu; mtu ambaye atatimiza yale yote ninayotaka kuyatenda.’ Kutokana na ukoo wake mtu huyu, Mungu, kama alivyoahidi, amewapelekea watu wa Israeli Mwokozi, ndiye Yesu. Kabla ya kuja kwake Yesu, Yohane alimtangulia akiwahubiria watu wote wa Israeli kwamba ni lazima watubu na kubatizwa. Yohane alipokuwa anamaliza ujumbe wake aliwaambia watu: ‘Mnadhani mimi ni nani? Mimi si yule mnayemtazamia. Huyo anakuja baada yangu na mimi sistahili hata kuzifungua kamba za viatu vyake.’ “Ndugu, nyinyi mlio watoto wa ukoo wa Abrahamu, na wengine wote mnaomcha Mungu! Ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. Kwa maana wenyeji wa Yerusalemu na wakuu wao hawakumtambua yeye kuwa Mwokozi, wala hawakuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato. Hata hivyo, waliyafanya maneno ya manabii yatimie kwa kumhukumu Yesu adhabu ya kifo. Ingawa hawakumpata na hatia inayostahili auawe, walimwomba Pilato amhukumu auawe. Na baada ya kutekeleza yote yaliyokuwa yameandikwa kumhusu yeye, walimshusha kutoka msalabani, wakamweka kaburini. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Naye, kwa siku nyingi, aliwatokea wale waliofuatana naye kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu wa Israeli. Nasi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema: Jambo lile Mungu alilowaahidia babu zetu, amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili: ‘Wewe ni Mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako.’ Na juu ya kumfufua kutoka kwa wafu, asipate tena kurudi huko na kuoza, Mungu alisema hivi: ‘Nitakupa baraka takatifu na za kweli nilizomwahidia Daudi.’ Naam, na katika sehemu nyingine za Zaburi asema: ‘Hutamwacha Mtakatifu wako aoze.’ Sasa, Daudi mwenyewe alitimiza matakwa ya Mungu wakati wake; kisha akafa na kuzikwa karibu na wazee wake, na mwili wake ukaoza. Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu hakupata kuoza. Kwa hiyo, jueni, ndugu zangu, kwamba kwa njia ya mtu huyu ujumbe kuhusu kusamehewa dhambi unahubiriwa kwenu; na ya kwamba kila mmoja anayemwamini Yesu anasamehewa dhambi zote, jambo ambalo halingewezekana kwa njia ya sheria. Jihadharini basi, msije mkapatwa na yale yaliyosemwa na manabii: ‘Sikilizeni enyi wenye madharau, shangaeni mpotee! Kwa maana kitu ninachofanya sasa, nyakati zenu, ni kitu ambacho hamtakiamini hata kama mtu akiwaelezeni.’” Paulo na Barnaba walipokuwa wanatoka katika lile sunagogi, wale watu waliwaalika waje tena siku ya Sabato iliyofuata, waongee zaidi juu ya mambo hayo. Mkutano huo ulipomalizika, Wayahudi wengi na watu wa mataifa mengine waliokuwa wameongokea dini ya Kiyahudi waliwafuata Paulo na Barnaba. Hao mitume waliongea nao, wakawatia moyo waendelee kuishi wakitegemea neema ya Mungu. Siku ya Sabato iliyofuata, karibu kila mtu katika ule mji alikuja kusikiliza neno la Bwana. Lakini Wayahudi walipoliona hilo kundi la watu walijaa wivu, wakapinga alichokuwa anasema Paulo na kumtukana. Hata hivyo, Paulo na Barnaba waliongea kwa uhodari zaidi, wakasema, “Ilikuwa ni lazima neno la Mungu liwafikieni nyinyi kwanza; lakini kwa kuwa mmelikataa na kujiona hamstahili uhai wa milele, basi, tunawaacheni na kuwaendea watu wa mataifa mengine. Maana Bwana alituagiza hivi: ‘Nimekuweka wewe uwe mwanga kwa watu wa mataifa, ili uwaletee watu wokovu pote ulimwenguni.’” Watu wa mataifa mengine waliposikia jambo hilo walifurahi, wakausifu ujumbe wa Mungu; na wale waliokuwa wamechaguliwa kupata uhai wa milele, wakawa waumini. Neno la Bwana likaenea kila mahali katika sehemu ile. Lakini Wayahudi waliwachochea wanawake wa tabaka ya juu wa mataifa mengine ambao walikuwa wacha Mungu, na wanaume maarufu wa mji huo. Wakaanza kuwatesa Paulo na Barnaba, wakawafukuza kutoka katika eneo lao. Basi, mitume wakayakunguta mavumbi yaliyokuwa katika miguu yao kama onyo, kisha wakaenda Ikonio. Lakini hao wafuasi walikuwa wamejaa furaha na Roho Mtakatifu. Kule Ikonio, mambo yalikuwa kama yalivyokuwa kule Antiokia; Paulo na Barnaba walikwenda katika sunagogi la Wayahudi wakaongea kwa uhodari hata Wayahudi wengi na Wagiriki wakawa waumini. Lakini Wayahudi wengine waliokataa kuwa waumini walichochea na kutia chuki katika mioyo ya watu wa mataifa mengine ili wawapinge hao ndugu. Paulo na Barnaba waliendelea kukaa huko kwa muda mrefu. Waliongea kwa uhodari juu ya Bwana, naye Bwana akathibitisha ukweli wa ujumbe walioutoa juu ya neema yake, kwa kuwawezesha kutenda miujiza na maajabu. Watu wa mji huo waligawanyika: Wengine waliwaunga mkono Wayahudi, na wengine walikuwa upande wa mitume. Mwishowe, baadhi ya watu wa mataifa mengine na Wayahudi, wakishirikiana na wakuu wao, waliazimu kuwatendea vibaya hao mitume na kuwapiga mawe. Mitume walipogundua jambo hilo, walikimbilia Lustra na Derbe, miji ya Lukaonia, na katika sehemu za jirani, wakawa wanahubiri Habari Njema huko. Kulikuwa na mtu mmoja huko Lustra ambaye alikuwa kiwete tangu kuzaliwa, na alikuwa hajapata kutembea kamwe. Mtu huyo alikuwa anamsikiliza Paulo alipokuwa anahubiri. Paulo alimtazama kwa makini, na alipoona kuwa alikuwa na imani ya kuweza kuponywa, akasema kwa sauti kubwa, “Simama wima kwa miguu yako!” Huyo mtu aliyelemaa miguu akainuka ghafla, akaanza kutembea. Umati wa watu walipoona alichofanya Paulo, walianza kupiga kelele kwa lugha ya Kilukaonia: “Miungu imetujia katika sura za binadamu!” Barnaba akaitwa Zeu, na Paulo, kwa vile yeye ndiye aliyekuwa anaongea, akaitwa Herme. Naye kuhani wa hekalu la Zeu lililokuwa nje ya mji akaleta fahali na shada za maua mbele ya mlango mkuu wa mji, naye pamoja na ule umati wa watu akataka kuwatambikia mitume. Barnaba na Paulo walipopata habari hizo waliyararua mavazi yao na kukimbilia katika lile kundi la watu wakisema kwa sauti kubwa: “Ndugu, kwa nini mnafanya mambo hayo? Sisi pia ni binadamu kama nyinyi. Na, tuko hapa kuwahubirieni Habari Njema, mpate kuziacha hizi sanamu tupu, mkamgeukie Mungu aliye hai, Mungu aliyeumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo. Zamani Mungu aliruhusu kila taifa lifanye lilivyopenda. Hata hivyo, Mungu hakuacha kujidhihirisha kwa mambo mema anayowatendea: Huwanyeshea mvua toka angani, huwapa mavuno kwa wakati wake, huwapa chakula na kuijaza mioyo yenu furaha.” Ingawa walisema hivyo haikuwa rahisi kuwazuia wale watu wasiwatambikie. Lakini Wayahudi kadhaa walikuja kutoka Antiokia na Ikonio, wakawafanya watu wajiunge nao, wakampiga mawe Paulo na kumburuta hadi nje ya mji wakidhani amekwisha kufa. Lakini waumini walipokusanyika na kumzunguka, aliamka, akarudi mjini. Kesho yake, yeye pamoja na Barnaba walikwenda Derbe. Baada ya Paulo na Barnaba kuhubiri Habari Njema huko Derbe na kupata wafuasi wengi, walifunga safari kwenda Antiokia kwa kupitia Lustra na Ikonio. Waliwaimarisha waumini wa miji hiyo na kuwatia moyo wabaki imara katika imani. Wakawaambia, “Ni lazima sisi sote kupitia katika taabu nyingi ili tuingie katika ufalme wa Mungu.” Waliteua wazee katika kila kanisa kwa ajili ya waumini, kisha, kwa kusali na kufunga, wakawaweka chini ya ulinzi wa Bwana ambaye walikuwa wanamwamini. Baada ya kupitia katika nchi ya Pisidia, walifika Pamfulia. Baada ya kuhubiri ule ujumbe huko Perga, walikwenda Atalia. Kutoka huko walisafiri kwa meli wakarudi Antiokia ambako hapo awali walikuwa wamewekwa chini ya ulinzi wa neema ya Mungu kwa ajili ya kazi ambayo sasa walikuwa wameitimiza. Walipofika huko Antiokia walifanya mkutano wa kanisa la mahali hapo, wakawapa taarifa juu ya mambo Mungu aliyofanya pamoja nao, na jinsi alivyowafungulia watu wa mataifa mengine mlango wa kuingia katika imani. Wakakaa pamoja na wale waumini kwa muda mrefu. Basi, watu wengine walifika Antiokia kutoka Yudea wakaanza kuwafundisha wale ndugu wakisema, “Kama hamtatahiriwa kufuatana na mapokeo kama alivyoamuru Mose, hamtaweza kuokolewa.” Jambo hili lilisababisha ubishi mkubwa, na baada ya Paulo na Barnaba kujadiliana nao, ikaamuliwa Paulo na Barnaba pamoja na waumini kadhaa wa lile kanisa la Antiokia waende Yerusalemu kuwaona wale mitume na wazee kuhusu jambo hilo. Basi, kanisa liliwaaga, nao walipokuwa wanapitia Foinike na Samaria waliwaeleza watu jinsi mataifa mengine yalivyomgeukia Mungu. Habari hizo zikawafurahisha sana ndugu hao wote. Walipofika Yerusalemu walikaribishwa na kanisa, mitume na wazee; nao wakawapa taarifa juu ya yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao. Lakini waumini wengine waliokuwa wa kikundi cha Mafarisayo walisimama, wakasema, “Ni lazima watu wa mataifa mengine watahiriwe na kufundishwa kuifuata sheria.” Basi, mitume na wazee walifanya mkutano maalumu wa kuchunguza jambo hilo. Baada ya majadiliano marefu, Petro alisimama, akasema, “Ndugu zangu, nyinyi mnafahamu kwamba hapo awali Mungu alipenda kunichagua mimi miongoni mwenu nitangaze Habari Njema kwa watu wa mataifa, wapate kusikia na kuamini. Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi. Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani. Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba? Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tutaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu.” Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo wakieleza miujiza na maajabu ambayo Mungu alitenda kwa mikono yao kati ya watu wa mataifa mengine. Walipomaliza kuongea, Yakobo alianza kusema: “Ndugu zangu, nisikilizeni! Simoni ameeleza jinsi Mungu hapo awali alivyojishughulisha na watu wa mataifa mengine, akachagua baadhi yao wawe watu wake. Jambo hili ni sawa kabisa na maneno ya manabii, kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: ‘Baada ya mambo haya nitarudi, na kujenga tena kile kibanda cha Daudi kilichoanguka; nitayatengeneza magofu yake na kukijenga tena. Hapo watu wengine wote, watu wa mataifa yote niliowaita wawe wangu, watamtafuta Bwana. Ndivyo asemavyo Bwana, aliyefanya jambo hili lijulikane tangu kale.’ “Kwa hiyo, uamuzi wangu ni huu: Tusiwataabishe watu wa mataifa wanaomgeukia Mungu. Bali tuwapelekee barua kuwaambia wasile vyakula vilivyotiwa unajisi kwa kutambikiwa vinyago vya miungu; wajiepushe na uasherati; wasile mnyama yeyote aliyenyongwa, na wasinywe damu. Kwa maana kwa muda mrefu maneno ya Mose yamekuwa yakihubiriwa katika kila mji na kusomwa katika masunagogi yote kila siku ya Sabato.” Mitume, wazee na kanisa lote waliamua kuwachagua watu fulani miongoni mwao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Basi, wakamchagua Yuda aitwaye pia Barsaba, na Sila ambao wote walikuwa wanajulikana zaidi kati ya ndugu. Wakawapa barua hii: “Sisi mitume na wazee, ndugu zenu, tunawasalimuni nyinyi ndugu wa mataifa mengine mlioko huko Antiokia, Siria na Kilikia. Tumesikia kwamba watu wengine kutoka huku kwetu waliwavurugeni kwa maneno yao, wakaitia mioyo yenu katika wasiwasi. Lakini wamefanya hivyo bila ya idhini yoyote kutoka kwetu. Hivyo, tumeamua kwa pamoja kuwachagua watu kadhaa na kuwatuma kwenu pamoja na wapenzi wetu Barnaba na Paulo, ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo, tunawatuma Yuda na Sila kwenu; hawa watawaambieni wao wenyewe haya tuliyoandika. Basi, Roho Mtakatifu na sisi tumekubali tusiwatwike mzigo zaidi ya mambo haya muhimu: Msile vyakula vilivyotambikiwa vinyago; msinywe damu; msile nyama ya mnyama aliyenyongwa; na mjiepushe na uasherati. Mtakuwa mmefanya vema kama mkiepa kufanya mambo hayo. Wasalaam!” Baada ya kuwaaga, hao wajumbe walielekea Antiokia ambako waliita mkutano wa waumini, wakawapa hiyo barua. Walipoisoma hiyo barua, maneno yake yaliwatia moyo, wakafurahi sana. Yuda na Sila, ambao nao walikuwa manabii, walizungumza na hao ndugu kwa muda mrefu wakiwatia moyo na kuwaimarisha. Baada ya kukaa huko kwa muda fulani, ndugu wa Antiokia waliwaaga wakiwatakia amani, kisha wakarudi kwa wale waliokuwa wamewatuma. [ Lakini Sila aliamua kubaki.] Paulo na Barnaba walibaki huko Antiokia kwa muda; wakafundisha na kuhubiri neno la Bwana, pamoja na watu wengine wengi. Baada ya siku kadhaa, Paulo alimwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee wale ndugu katika kila mji tulikolihubiri neno la Bwana, tukajionee jinsi wanavyoendelea.” Barnaba alitaka wamchukue pia Yohane aitwaye Marko. Lakini Paulo hakupendelea kumchukua Marko, ambaye awali aliwaacha kule Pamfulia na kukataa kushiriki katika kazi yao. Basi, kukatokea ubishi mkali kati yao, wakaachana. Barnaba akamchukua Marko, wakapanda meli kwenda Kupro. Naye Paulo akamchagua Sila, na baada ya ndugu wa mahali hapo kumweka chini ya ulinzi wa neema ya Bwana, akaondoka. Katika safari hiyo alipitia Siria na Kilikia, akiyaimarisha makanisa. Paulo alifika Derbe na Lustra, ambako aliishi mfuasi mmoja aitwaye Timotheo. Mama yake ambaye pia alikuwa mfuasi, alikuwa Myahudi; lakini baba yake alikuwa Mgiriki. Timotheo alikuwa na sifa kubwa kati ya wale ndugu wa Lustra na Ikonio. Paulo alitaka Timotheo aandamane naye safarini, kwa hiyo alimtahiri. Alifanya hivyo kwa sababu Wayahudi wote walioishi sehemu hizo walijua kwamba baba yake Timotheo alikuwa Mgiriki. Walipokuwa wanapita katika ile miji waliwapa watu yale maagizo yaliyotolewa na mitume na wazee kule Yerusalemu, wakawaambia wayazingatie. Hivyo, yale makanisa yalizidi kuwa imara katika imani, na idadi ya waumini ikaongezeka kila siku. Walipitia sehemu za Frugia na Galatia kwani Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuhubiri huo ujumbe mkoani Asia. Walipofika kwenye mipaka ya Musia, walijaribu kuingia mkoani Bithunia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. Basi, walipitia Musia, wakaenda moja kwa moja mpaka Troa. Usiku huo, Paulo aliona maono ambayo alimwona mtu mmoja wa Makedonia amesimama pale na kumwomba: “Vuka, uje Makedonia ukatusaidie.” Mara baada ya Paulo kuona maono hayo, tulijitayarisha kwenda Makedonia bila kukawia, tukiwa na hakika kwamba Mungu ametuita tuwahubirie Habari Njema. Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli. Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa. Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo. Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema. Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, “Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae.” Akatuhimiza twende. Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake. Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, “Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu.” Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, “Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!” Mara huyo pepo akamtoka. Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu. Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, “Watu hawa ni Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu. Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata.” Kundi la watu likajiunga likawashambulia; na wale mahakimu wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakaamuru wapigwe viboko. Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali. Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo. Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza. Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana. Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka, na hivyo akauchomoa upanga wake, akataka kujiua. Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: “Usijidhuru mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa.” Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka kwa hofu. Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, “Waheshimiwa, nifanye nini nipate kuokoka?” Wao wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa pamoja na jamaa yako yote.” Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa yake. Yule askari aliwachukua saa ileile ya usiku akawasafisha majeraha yao, kisha yeye na jamaa yake wakabatizwa papo hapo. [ Halafu akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake, akawapa chakula. Yeye na jamaa yake yote wakafanya sherehe kwa vile sasa walikuwa wanamwamini Mungu]. Kesho yake asubuhi, mahakimu waliwatuma maofisa wao wakisema, “Wafungueni wale watu.” Yule askari wa gereza alimpasha habari Paulo: “Mahakimu wametuma ujumbe ili mfunguliwe. Sasa mnaweza kutoka na kwenda zenu kwa amani.” Lakini Paulo alimjibu, “Ati nini? Ingawa hatukuwa na kosa, walitupiga viboko hadharani hali sisi ni raia wa Roma. Tena, walitutia ndani na sasa wanataka kutufungulia kwa siri! Hata kidogo! Ni lazima wao wenyewe waje hapa watufungulie.” Hao maofisa waliwapasha habari mahakimu juu ya jambo hilo, nao waliposikia kwamba Paulo na Sila walikuwa raia wa Roma, waliogopa. Hivyo, walikwenda kuwataka radhi na baada ya kuwatoa ndani waliwaomba watoke katika mji ule. Paulo na Sila walitoka gerezani, wakaenda nyumbani kwa Ludia. Huko walionana na ndugu waumini na baada ya kuwatia moyo wakaondoka. Kwa kupitia Amfipoli na Apolonia, walisafiri mpaka Thesalonike ambako kulikuwa na sunagogi la Wayahudi. Paulo alijiunga nao kama ilivyokuwa desturi yake, akajadiliana nao Sabato tatu mfululizo, akitumia Maandiko Matakatifu. Aliyaeleza na kuonesha kwamba ilimbidi Kristo kuteswa na kufufuka kutoka kwa wafu. Akawaambia, “Yesu ambaye mimi namhubiri kwenu ndiye Kristo.” Baadhi yao walikubali wakajiunga na Paulo na Sila. Kadhalika, idadi kubwa ya Wagiriki waliomcha Mungu pamoja na wanawake wengi wa tabaka la juu, walijiunga nao. Lakini Wayahudi wakaona wivu; wakawakodi wafidhuli sokoni, wakafanya kikundi na kuzusha fujo mjini kote. Wakaivamia nyumba ya Yasoni wakitumaini kuwapata humo Paulo na Sila ili wawalete hadharani. Lakini hawakuwapata na hivyo walimburuta Yasoni pamoja na ndugu wengine mpaka kwa wakuu wa mji, wakapiga kelele: “Watu hawa wamekuwa wakivuruga dunia yote na sasa wako hapa mjini. Yasoni amewakaribisha nyumbani kwake. Wote wanafanya kinyume cha amri ya Kaisari wakisema eti: ‘Kuna mfalme mwingine aitwaye Yesu.’” Kwa maneno hayo waliwatia wasiwasi wakuu wa mji na kundi la watu. Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha wakawaacha waende zao. Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi. Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa Thesalonike. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila yalikuwa kweli. Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa tabaka la juu na wanaume pia. Lakini, Wayahudi wa Thesalonike walipogundua kwamba Paulo alikuwa anahubiri neno la Mungu huko Berea, walikwenda huko, wakaanza kufanya fujo na kuchochea makundi ya watu. Wale ndugu wakamsindikiza haraka aende pwani lakini Sila na Timotheo walibaki Berea. Wale ndugu waliomsindikiza Paulo walikwenda pamoja naye mpaka Athene. Kisha, wakarudi pamoja na maagizo kutoka kwa Paulo kwamba Sila na Timotheo wamfuate upesi iwezekanavyo. Paulo alipokuwa anawasubiri Sila na Timotheo huko Athene, moyo wake ulighadhibika sana alipoona jinsi mji huo ulivyokuwa umejaa sanamu za miungu. Alijadiliana na Wayahudi na watu wengine waliomcha Mungu katika sunagogi; na kila siku alikuwa na majadiliano mahali pa hadhara pamoja na wote wale waliojitokeza. Wengine waliofuata falsafa ya Epikuro na Stoiki walibishana naye. Wengine walisema, “Anataka kusema nini huyu bwanamaneno?” Kwa kuwa Paulo alikuwa anahubiri juu ya Yesu na juu ya ufufuo, wengine walisema, “Inaonekana kama anahubiri juu ya miungu ya kigeni.” Hivyo walimchukua Paulo, wakampeleka Areopago, wakasema, “Tunataka kujua jambo hili jipya ulilokuwa unazungumzia. Vitu vingine tulivyosikia kwa masikio yetu vinaonekana kuwa viroja kwetu. Tungependa kujua mambo haya yana maana gani.” Wananchi wa Athene na wakazi wengine wa huko walikuwa wanatumia wakati wao wote kuhadithiana na kusikiliza habari mpyampya. Basi, Paulo alisimama mbele ya baraza la Areopago, akasema, “Wananchi wa Athene! Ninaona kwamba nyinyi, kwa vyovyote, ni watu wa dini sana, maana nilipokuwa napita huko na huko nikiangalia sanamu zenu za ibada niliona madhabahu moja ambayo imeandikwa: ‘Kwa Mungu asiyejulikana.’ Basi, huyo mnayemwabudu bila kujua, ndiye ninayemhubiri kwenu. Mungu, aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo, ni Bwana wa mbingu na dunia; yeye hakai katika hekalu zilizojengwa na watu. Wala hatumikiwi kwa mikono ya watu kana kwamba anahitaji chochote kile, kwa maana yeye mwenyewe ndiye anayewapa watu uhai, anawawezesha kupumua na kuwapa kila kitu. Kutokana na mtu mmoja aliumba mataifa yote na kuyawezesha kuishi duniani kote. Aliamua na kupanga kabla kabisa lini na wapi mataifa hayo yangeishi. Alifanya hivyo, ili mataifa hayo yapate kumfuata, na kama vile kwa kupapasapapasa, yapate kumfikia. Hata hivyo lakini, Mungu hayuko mbali na kila mmoja wetu. Kama alivyosema mtu mmoja: ‘Ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu, na tuko!’ Ni kama washairi wenu wengine walivyosema: ‘Sisi ni watoto wake.’ Ikiwa basi, sisi ni watoto wa Mungu, haifai kumfikiria Mungu kuwa kama dhahabu, fedha au hata jiwe lililochongwa na kutiwa nakshi na binadamu. Mungu alifanya kana kwamba haoni nyakati zile watu walipokuwa wajinga. Lakini sasa, anaamuru watu wote kila mahali watubu. Kwa maana amekwisha weka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki kwa njia ya mtu mmoja aliyemteua. Mungu amewathibitishia wote jambo hili kwa kumfufua mtu huyo kutoka kwa wafu!” Walipomsikia Paulo anasema juu ya jambo la kufufuka kwa wafu, wengine wao waliangua kicheko; lakini wengine walisema, “Tunataka kukusikia tena juu ya jambo hili!” Hivyo, Paulo aliwaacha, akatoka barazani. Lakini watu kadhaa waliandamana naye, wakawa waumini. Miongoni mwao walikuwa Dionisio wa Areopago, na mwanamke mmoja aitwaye Damari na wengineo. Baada ya hayo, Paulo aliondoka Athene, akaenda Korintho. Huko Korintho, alimkuta Myahudi mmoja aitwaye Akula, mzaliwa wa Ponto. Akula pamoja na mkewe aitwaye Priskila, walikuwa wamerudi kutoka Italia siku hizohizo kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Roma. Paulo alikwenda kuwaona, na kwa vile wao walikuwa mafundi wa kushona mahema kama yeye, Paulo alikaa nao akafanya kazi. Kila Sabato alifanya majadiliano katika sunagogi akijaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki. Baada ya Sila na Timotheo kuwasili kutoka Makedonia, Paulo alianza kutumia wakati wake wote kwa ajili ya kuhubiri, akawathibitishia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo. Walipompinga na kuanza kumtukana, aliyakunguta mavazi yake mbele yao akisema, “Mkipotea ni shauri lenu wenyewe; mimi sina lawama yoyote juu ya jambo hilo. Na tangu sasa nitawaendea watu na mataifa mengine.” Basi, akatoka hapo akaenda kukaa nyumbani kwa mtu mmoja mcha Mungu aitwaye Tito Yusto, ambaye nyumba yake ilikuwa karibu na lile sunagogi. Krispo, mkuu wa hilo sunagogi, alimwamini Bwana yeye pamoja na jamaa yake yote. Wakorintho wengi waliusikiliza ujumbe huo, wakaamini na kubatizwa. Siku moja usiku, Bwana alimwambia Paulo katika maono: “Usiogope, endelea kuhubiri tu bila kufa moyo, maana mimi niko pamoja nawe. Hakuna mtu atakayejaribu kukudhuru maana hapa mjini pana watu wengi walio upande wangu.” Basi, Paulo alikaa huko akifundisha neno la Mungu kati yao kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Lakini wakati Galio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Akaya, Wayahudi walimvamia Paulo kwa pamoja na kumpeleka mahakamani. Wakasema, “Tunamshtaki mtu huyu kwa sababu ya kuwashawishi watu wamwabudu Mungu kwa namna inayopingana na sheria.” Kabla tu Paulo hajaanza kusema, Galio aliwaambia Wayahudi, “Sikilizeni enyi Wayahudi! Kama kweli jambo hili lingekuwa juu ya uhalifu au uovu ningekuwa tayari kuwasikilizeni. Lakini kama ni shauri la ubishi kuhusu maneno na majina na sheria yenu, amueni nyinyi wenyewe. Mimi sitaki kuwa hakimu wa mambo hayo!” Basi, akawafukuza kutoka mahakamani. Nao wote wakamkamata Sosthene ambaye alikuwa kiongozi wa sunagogi, wakampiga palepale mbele ya mahakama. Lakini Galio hakujali kitendo hicho hata kidogo. Paulo alikaa bado na wale ndugu huko Korintho kwa siku nyingi. Kisha aliwaaga, akapanda meli kwenda Siria pamoja na Priskila na Akula. Huko Kenkrea, alinyoa nywele zake kwa sababu ya nadhiri aliyokuwa ameweka. Walifika Efeso na hapo Paulo aliwaacha Priskila na Akula, akaenda katika sunagogi, akajadiliana na Wayahudi. Walimwomba akae nao muda mrefu zaidi, lakini hakupenda. Bali alipokuwa anaondoka, alisema, “Mungu akipenda nitakuja kwenu tena.” Akaondoka Efeso kwa meli. Meli ilitia nanga Kaisarea, naye Paulo akaenda Yerusalemu kulisalimia lile kanisa, kisha akaenda Antiokia. Alikaa huko muda mfupi, halafu akaendelea na safari kwa kupitia sehemu za Galatia na Frugia akiwatia moyo wafuasi wote. Myahudi mmoja aitwaye Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, alifika Efeso. Alikuwa mtu mwenye ufasaha wa kuongea na mwenye ujuzi mkubwa wa Maandiko Matakatifu. Alikuwa amefundishwa juu ya hiyo njia ya Bwana, na akiwa motomoto, aliongea juu ya habari za Yesu akafundisha kwa usahihi ingawa alikuwa amepata ubatizo wa Yohane tu. Priskila na Akula walipomsikia akiongea kwa uhodari ndani ya sunagogi, walimchukua kwao wakamfundisha hiyo njia ya Mungu kwa usahihi zaidi. Apolo alipoamua kwenda Akaya, wale ndugu walimtia moyo kwa kuwaandikia wafuasi kule Akaya wampokee. Alipofika huko, aliweza kwa msaada wa neema ya Mungu, kuwasaidia sana wale ndugu waliopata kuwa waumini; kwa maana aliendelea kwa uhodari kuwashinda Wayahudi hadharani akithibitisha kwa Maandiko Matakatifu kuwa Yesu ni Kristo. Wakati Apolo alipokuwa Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso ambako aliwakuta wanafunzi kadhaa. Akauliza, “Je, mlipopata kuwa waumini mlipokea Roho Mtakatifu?” Nao wakamjibu, “La! Hata hatujasikia kwamba kuna Roho Mtakatifu.” Naye akasema, “Sasa mlipata ubatizo wa namna gani?” Wakamjibu, “Ubatizo wa Yohane.” Naye Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohane ulikuwa wa kuonesha kwamba watu wametubu. Yohane aliwaambia watu wamwamini yule ambaye alikuwa anakuja baada yake, yaani Yesu.” Baada ya kusikia hayo, walibatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Basi, Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akawashukia, wakaanza kusema lugha ngeni na kutangaza ujumbe wa Mungu. Wote jumla walikuwa watu wapatao kumi na wawili. Kwa muda wa miezi mitatu Paulo alikuwa akienda katika sunagogi, akawa na majadiliano ya kuvutia sana juu ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikuwa wakaidi, wakakataa kuamini, wakaanza kuongea vibaya juu ya hiyo njia ya Bwana katika kusanyiko la watu. Hapo Paulo alivunja uhusiano nao, akawachukua pembeni wale wanafunzi wake, akawa anazungumza nao kila siku katika jumba la masomo la Turano. Aliendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka miwili hata wakazi wote wa Asia, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, wakaweza kusikia neno la Bwana. Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo. Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia, wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao; na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao. Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya walisafiri huko na huko wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: “Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri.” Watoto saba wa Skewa, kuhani mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mbaya aliwajibu, “Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini nyinyi ni nani?” Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha. Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu. Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda. Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande 50,000 vya fedha. Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi. Baada ya mambo hayo, Paulo aliamua kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Alisema, “Baada ya kufika huko, itanilazimu kuona Roma pia.” Hivyo, aliwatuma wawili wa wasaidizi wake, Timotheo na Erasto, wamtangulie kwenda Makedonia, naye akabaki kwa muda huko Asia. Wakati huo ndipo kulipotokea ghasia kubwa huko Efeso kwa sababu ya hiyo njia ya Bwana. Kulikuwa na mfua fedha mmoja aitwaye Demetrio, ambaye alikuwa na kazi ya kutengeneza sanamu za nyumba ya mungu wa kike aitwaye Artemi. Shughuli hiyo iliwapatia mafundi wake faida kubwa. Demetrio aliwakusanya hao wafanyakazi pamoja na wengine waliokuwa na kazi kama hiyo, akawaambia, “Wananchi, mnafahamu kwamba kipato chetu kinatokana na biashara hii. Sasa, mnaweza kusikia na kujionea wenyewe mambo Paulo anayofanya, si hapa Efeso tu, ila pia kote katika Asia. Yeye amewashawishi na kuwageuza watu wakakubali kwamba miungu ile iliyotengenezwa na watu si miungu hata kidogo. Hivyo iko hatari kwamba biashara yetu itakuwa na jina baya. Si hivyo tu, bali pia jambo hilo linaweza kuifanya nyumba ya mungu Artemi kuwa si kitu cha maana. Hatimaye sifa zake huyo ambaye Asia na dunia yote inamwabudu, zitakwisha.” Waliposikia hayo, waliwaka hasira, wakaanza kupiga kelele: “Mkuu ni Artemi wa Efeso!” Mji wote ukajaa ghasia. Wakawavamia Gayo na Aristarko, wenyeji wa Makedonia, ambao walikuwa wasafiri wenzake Paulo, wakakimbia nao mpaka kwenye ukumbi wa michezo. Paulo mwenyewe alitaka kuukabili huo umati wa watu, lakini wale waumini walimzuia. Maofisa wengine wa huo mkoa wa Asia, waliokuwa rafiki zake, walimpelekea Paulo ujumbe wakimsihi asijihatarishe kwa kwenda kwenye ukumbi wa michezo. Wakati huo, kila mtu alikuwa anapayuka; wengine hili na wengine lile, mpaka hata ule mkutano ukavurugika. Wengi hawakujua hata sababu ya kukutana kwao. Kwa vile Wayahudi walimfanya Aleksanda ajitokeze mbele, baadhi ya watu katika ule umati walidhani kuwa ndiye. Basi, Aleksanda aliwaashiria watu kwa mkono akitaka kujitetea mbele ya ule umati wa watu. Lakini walipotambua kuwa yeye ni Myahudi, wote kwa sauti moja walipiga kelele: “Mkuu ni Artemi wa Efeso!” Wakaendelea kupayukapayuka hivyo kwa muda wa saa mbili. Hatimaye karani wa mji alifaulu kuwanyamazisha, akawaambia, “Wananchi wa Efeso, kila mtu anajua kwamba mji huu wa Efeso ni mlinzi wa nyumba ya mungu Artemi na mlinzi wa ile sanamu iliyoanguka kutoka mbinguni. Hakuna anayeweza kukana mambo hayo. Hivyo basi, tulieni; msifanye chochote bila hadhari. Mmewaita watu hawa hapa ingawaje hawakuikufuru nyumba ya mungu wala kumtukana mungu wetu wa kike. Kama, basi Demetrio na wafanyakazi wake wana mashtaka yao kuhusu watu hawa, yapo mahakama na wakuu wa mikoa; wanaweza kushtakiana huko. Kama mna matatizo mengine, yapelekeni katika kikao halali. Kwa maana tungaliweza kushtakiwa kwa kusababisha ghasia kutokana na vituko vya leo. Ghasia hii haina msingi halali na hatungeweza kutoa sababu za kuridhisha za ghasia hiyo.” Baada ya kusema hayo, aliuvunja mkutano. Ile ghasia ya Efeso ilipokwisha tulia Paulo aliwaita pamoja wale waumini, akawatia moyo. Kisha akawaaga, akasafiri kwenda Makedonia. Alipitia sehemu za nchi zile akiwatia watu moyo kwa maneno mengi. Halafu akafika Ugiriki ambako alikaa kwa miezi mitatu. Alipokuwa anajitayarisha kwenda Siria, aligundua kwamba Wayahudi walikuwa wanamfanyia mpango mbaya; hivyo aliamua kurudi kwa kupitia Makedonia. Sopatro, mwana wa Pirho, kutoka Berea, aliandamana naye; pia Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike, Gayo kutoka Derbe, Timotheo, Tukiko na Trofimo wa mkoa wa Asia. Hao walitutangulia na kutungojea kule Troa. Sisi, baada ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, tulipanda meli kutoka Filipi na baada ya siku tatu tukawafikia kule Troa. Huko tulikaa kwa muda wa juma moja. Jumamosi jioni tulikutana ili kumega mkate. Kwa vile Paulo alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliwahutubia watu na kuendelea kuongea nao hadi usiku wa manane. Katika chumba tulimokuwa, ghorofani, kulikuwa na taa nyingi zinawaka. Kijana mmoja aitwaye Eutuko alikuwa ameketi dirishani wakati Paulo alipokuwa anaendelea kuhutubu. Eutuko alianza kusinzia kidogokidogo na hatimaye usingizi ukambana, akaanguka chini kutoka ghorofa ya tatu. Wakamwokota amekwisha kufa. Lakini Paulo alishuka chini, akainama, akamkumbatia na kusema, “Msiwe na wasiwasi maana kuna uhai bado ndani yake.” Kisha akapanda tena ghorofani, akamega mkate, akala. Aliendelea kuhubiri kwa muda mrefu hadi alfajiri, halafu akaondoka. Wale watu walimchukua yule kijana hadi nyumbani akiwa mzima kabisa, wakapata kitulizo kikubwa. Sisi tulipanda meli tukatangulia kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Ndivyo alivyopanga; maana alitaka kufika huko kwa kupitia nchi kavu. Basi, alitukuta kule Aso, tukampandisha melini, tukaenda Mitulene. Kutoka huko tulisafiri tukafika Kio kesho yake. Siku ya pili, tulitia nanga Samo na kesho yake tukafika Mileto. Paulo alikuwa amekusudia kuendelea na safari kwa meli bila kupitia Efeso ili asikawie zaidi huko Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste kama ingewezekana. Kutoka Mileto Paulo alituma ujumbe kwa wazee wa Efeso wakutane naye. Walipofika kwake aliwaambia, “Mnajua jinsi nilivyokaa nanyi siku zote tangu siku ile ya kwanza nilipofika Asia. Mnajua jinsi nilivyomtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, kwa machozi na matatizo yaliyonipata kutokana na mipango ya hila ya Wayahudi. Mnajua kwamba sikusita hata kidogo kuwahubiria hadharani na nyumbani mwenu na kuwafundisha chochote ambacho kingewasaidieni. Niliwaonya wote — Wayahudi, kadhalika na watu wa mataifa, wamgeukie Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu. Sasa, sikilizeni! Mimi, nikiwa ninamtii Roho, nakwenda Yerusalemu bila kufahamu yatakayonipata huko. Ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu ananithibitishia katika kila mji kwamba vifungo na mateso ndivyo vinavyoningojea. Lakini, siuthamini uhai wangu kuwa kitu sana kwangu mradi tu nikamilishe ule utume wangu na ile kazi aliyonipa Bwana Yesu niifanye, yaani nishuhudie Habari Njema ya neema ya Mungu. “Nimepita miongoni mwenu nyote nikiuhubiri ufalme wa Mungu. Sasa lakini, najua hakuna hata mmoja wenu atakayeniona tena. Hivyo, leo hii ninawathibitishieni rasmi kwamba ikijatokea akapotea mmoja wenu, mimi sina lawama yoyote. Kwa maana sikusita hata kidogo kuwatangazieni azimio lote la Mungu. Jihadharini wenyewe; lilindeni lile kundi ambalo Roho Mtakatifu amewaweka nyinyi muwe walezi wake. Lichungeni kanisa la Mungu ambalo amejipatia kwa damu ya Mwanae. Nafahamu vizuri sana kwamba baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali watawavamieni, na hawatakuwa na huruma kwa kundi hilo. Hata kutoka miongoni mwenu watatokea watu ambao watasema mambo ya uongo ili kuwapotosha watu na kuwafanya wawafuate wao tu. Kwa hiyo, muwe macho mkikumbuka kwamba kwa muda wa miaka mitatu, usiku na mchana, sikuchoka kumwonya kila mmoja wenu kwa machozi. “Na sasa basi, ninawaweka nyinyi chini ya ulinzi wa Mungu na ujumbe wa neema yake. Yeye anao uwezo wa kuwajenga na kuwawezesha mzipate zile baraka alizowawekea watu wake. Mimi sikutamani hata mara moja fedha, wala dhahabu, wala nguo za mtu yeyote. Mnajua nyinyi wenyewe kwamba nimefanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe, ili kujipatia mahitaji yangu na ya wenzangu. Nimekuwa nikiwapeni daima mfano kwamba kwa kufanya kazi mithili hiyo tunapaswa kuwasaidia walio dhaifu, tukikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe: ‘Heri zaidi kutoa kuliko kupokea.’” Baada ya kusema hayo, Paulo alipiga magoti pamoja nao wote, akasali. Wote walikuwa wanalia, na kumwaga kwa kumkumbatia na kumbusu. Jambo lililowahuzunisha zaidi lilikuwa neno alilosema kwamba hawangemwona tena. Basi, wakamsindikiza hadi melini. Tulipokwisha agana nao, tulipanda meli tukaenda moja kwa moja mpaka Kosi. Kesho yake tulifika Rode, na kutoka huko tulikwenda Patara. Huko, tulikuta meli iliyokuwa inakwenda Foinike, hivyo tulipanda, tukasafiri. Baada ya kufika mahali ambapo tuliweza kuona Kupro, tulipitia upande wake wa kusini tukaelekea Siria. Tulitia nanga katika mji wa Tiro ambapo ile meli ilikuwa ipakuliwe shehena yake. Tulikuta waumini huko, tukakaa pamoja nao kwa muda wa juma moja. Waumini hao wakawa wanaongea kwa nguvu ya Roho, wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu. Lakini muda wetu ulipokwisha tuliondoka. Wote pamoja na wanawake na watoto wao walitusindikiza mpaka nje ya mji. Tulipofika pwani, sote tulipiga magoti tukasali. Kisha tuliagana; sisi tukapanda meli, nao wakarudi makwao. Sisi tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai ambapo tuliwasalimu ndugu zetu, tukakaa nao siku moja. Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisarea. Huko tulikwenda nyumbani kwa mhubiri Filipo. Yeye alikuwa mmoja wa wale saba waliochaguliwa kule Yerusalemu. Alikuwa na binti wanne ambao walikuwa na kipaji cha unabii. Baada ya kukaa huko siku kadhaa, nabii mmoja aitwaye Agabo alifika kutoka Yudea. Alitujia, akachukua mkanda wa Paulo, akajifunga mikono na miguu, akasema, “Roho Mtakatifu asema hivi: ‘Wayahudi kule Yerusalemu watamfunga namna hii mtu mwenye mkanda huu na kumtia mikononi mwa watu wa mataifa.’” Tuliposikia hayo, sisi na wale watu wengine waliokuwa hapo tulimsihi Paulo asiende Yerusalemu. Lakini yeye alijibu, “Mnataka kufanya nini? Mnataka kuvunja moyo wangu kwa machozi? Niko tayari siyo tu kutiwa ndani kule Yerusalemu, ila hata kufa kwa ajili ya Bwana Yesu.” Tuliposhindwa kumshawishi tulinyamaza, tukasema tu: “Atakalo Bwana lifanyike!” Baada ya kukaa pale kwa muda, tulifunga mizigo yetu, tukaendelea na safari kwenda Yerusalemu. Baadhi ya wale wafuasi wa Kaisarea walikwenda pamoja nasi, wakatupeleka nyumbani kwa Mnasoni ambaye tulikuwa tunakwenda kukaa naye kwa muda. Mnasoni alikuwa mwenyeji wa Kupro na alikuwa amekuwa mwaamini kwa siku nyingi. Tulipofika Yerusalemu, ndugu waumini walitupokea vizuri sana. Kesho yake Paulo alikwenda pamoja nasi kumwamkia Yakobo, na wazee wote wa kanisa walikuwapo pia. Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwapa taarifa kamili kuhusu yote Mungu aliyokuwa ametenda kati ya watu wa mataifa kwa njia ya utumishi wake. Waliposikia hayo, walimtukuza Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaweza kuona kwamba kuna maelfu ya Wayahudi ambao sasa wamekuwa waumini na wote hao wanazingatia sheria. Wamepata habari zako kwamba umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wanaoishi miongoni mwa watu wa mataifa mengine kuwa wasiijali sheria, wasiwatahiri watoto wao na kwamba wasizifuate mila za Wayahudi. Sasa, mambo yatakuwaje? Ni dhahiri kuwa watapata habari kwamba umekwisha wasili hapa. Basi, fanya kama tunavyokushauri. Tunao hapa watu wanne ambao wameweka nadhiri. Jiunge nao katika ibada ya kujitakasa, ukalipe na gharama zinazohusika, kisha wanyolewe nywele zao. Hivyo watu wote watatambua kwamba habari zile walizoambiwa juu yako hazina msingi wowote, na kwamba wewe binafsi bado unaishi kufuatana na maagizo ya sheria za Mose. Kuhusu wale watu wa mataifa mengine ambao wamekuwa waumini, tumekwisha wapelekea barua tukiwaambia mambo tuliyoamua: Wasile chochote kilichotambikiwa miungu ya uongo, wasinywe damu, wasile nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.” Basi, kesho yake Paulo aliwachukua wale watu akafanya ibada ya kujitakasa pamoja nao. Kisha akaingia hekaluni kutoa taarifa kuhusu mwisho wa siku za kujitakasa na kuhusu tambiko itakayotolewa kwa ajili ya kila mmoja wao. Wakati siku hizo saba zilipokaribia kuisha, Wayahudi waliokuwa wametoka katika mkoa wa Asia walimwona Paulo hekaluni. Basi, wakachochea hasira katika kundi lote la watu, wakamtia nguvuni wakipiga kelele: “Wananchi wa Israeli, msaada, msaada! Huyu ndiye yule mtu anayewafundisha watu kila mahali mambo yanayopinga watu wa Israeli, yanayopinga sheria ya Mose na mahali hapa patakatifu. Hata sasa amewaingiza watu wa mataifa mengine hekaluni na kupatia unajisi mahali hapa patakatifu.” Sababu ya kusema hivyo ni kwamba walikuwa wamemwona Trofimo, mwenyeji wa Efeso, akiwa pamoja na Paulo mjini, wakadhani kwamba Paulo alikuwa amemwingiza hekaluni. Mji wote ulienea ghasia; watu wakaja kutoka pande zote, wakamkamata Paulo, wakamburuta, wakamtoa nje ya hekalu, na papo hapo milango ya hekalu ikafungwa. Walikuwa tayari kumwua, lakini habari zilimfikia mkuu wa jeshi la Kiroma kuwa Yerusalemu yote ilikuwa imejaa ghasia. Mara, mkuu wa jeshi akawachukua askari na jemadari, akalikabili lile kundi la watu. Nao walipomwona mkuu wa jeshi na askari, wakaacha kumpiga Paulo. Mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamtia nguvuni na kuamuru afungwe minyororo miwili. Kisha akauliza, “Ni mtu gani huyu, na amefanya nini?” Wengine katika lile kundi la watu walikuwa wanapayuka kitu hiki na wengine kitu kingine. Kwa sababu ya ghasia hiyo, mkuu wa jeshi hakufaulu kujua kisa kamili. Hivyo, aliamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome. Paulo alipofika kwenye ngazi, askari walilazimika kumbeba kwa sababu ya fujo za watu. Kwa maana watu kundi kubwa walimfuata wakipiga kelele, “Mwulie mbali!” Walipokuwa wanamwingiza ndani ya ngome, Paulo alimwomba mkuu wa jeshi akisema, “Naweza kukuambia kitu?” Yule mkuu wa jeshi akamjibu, “Je, unajua Kigiriki? Kwani wewe si yule Mmisri ambaye hivi majuzi alianzisha uasi na kuwaongoza majahili 4,000 hadi jangwani?” Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia; mimi ni raia wa mji maarufu. Tafadhali, niruhusu niongee na watu.” Yule mkuu wa jeshi akamruhusu. Hivyo Paulo alisimama juu ya ngazi, akawapungia mkono wale watu, na walipokaa kimya, akaanza kuongea nao kwa Kiebrania: “Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni sasa nikijitetea mbele yenu!” Waliposikia akiongea nao kwa Kiebrania wakazidi kukaa kimya zaidi kuliko hapo awali. Naye Paulo akaendelea kusema, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia. Lakini nililelewa papa hapa mjini Yerusalemu chini ya mkufunzi Gamalieli. Nilifundishwa kufuata kwa uthabiti sheria ya wazee wetu. Nilijitolea kwa moyo wote kwa Mungu kama nyinyi wenyewe mlivyo hivi leo. Niliwatesa hata kuwaua wale watu waliofuata njia hii. Niliwatia nguvuni wanaume kwa wanawake na kuwafunga gerezani. Kuhani mkuu na baraza lote la wazee wanaweza kushuhudia jambo hilo. Kutoka kwao nilipokea barua walioandikiwa wale ndugu Wayahudi waliokuwa huko Damasko. Nilikwenda Damasko ili niwatie nguvuni watu hao na kuwaleta wamefungwa mpaka Yerusalemu ili waadhibiwe. “Basi, nilipokuwa njiani karibu na kufika Damasko, yapata saa sita mchana, mwanga mkubwa kutoka mbinguni ulitokea ghafla ukaniangazia pande zote. Hapo nilianguka chini, nikasikia sauti ikiniambia: ‘Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?’ Nami nikauliza, ‘Nani wewe, Bwana?’ Naye akaniambia, ‘Mimi ni Yesu wa Nazareti ambaye wewe unamtesa.’ Wale wenzangu waliuona ule mwanga lakini hawakusikia sauti ya yule aliyeongea nami. Basi, mimi nikauliza, ‘Nifanye nini Bwana?’ Naye Bwana akaniambia, ‘Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa kufanya.’ Kutokana na ule mwanga mkali sikuweza kuona na hivyo iliwabidi wale wenzangu kuniongoza kwa kunishika mkono mpaka nikafika Damasko. “Huko kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Anania, mtu mcha Mungu, mwenye kuitii sheria yetu na aliyeheshimika sana mbele ya Wayahudi waliokuwa wanaishi Damasko. Yeye alikuja kuniona, akasimama karibu nami, akasema, ‘Ndugu Saulo! Ona tena.’ Papo hapo nikaona tena, nikamwangalia. Halafu Anania akasema, ‘Mungu wa babu zetu amekuchagua upate kujua matakwa yake na kumwona yule mtumishi wake mwadilifu na kumsikia yeye mwenyewe akiongea. Kwa maana utamshuhudia kwa watu wote ukiwaambia yale uliyoyaona na kuyasikia. Sasa basi, ya nini kukawia zaidi? Simama, ubatizwe na kuondolewa dhambi zako kwa kuliungama jina lake.’ “Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali hekaluni, niliona maono. Nilimwona Bwana akiniambia, ‘Haraka! Ondoka Yerusalemu upesi kwa maana watu wa hapa hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.’ Nami nikamjibu, ‘Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga wale waliokuwa wanakuamini. Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya wale waliokuwa wanamuua.’ Naye Bwana akaniambia, ‘Nenda; nitakutuma mbali kwa mataifa mengine.’” Mpaka hapa, wale watu walikuwa wanamsikiliza, lakini aliposema maneno haya, walianza kusema kwa sauti kubwa, “Mwondoe duniani! Mtu wa namna hiyo hastahili kuishi.” Waliendelea kupayukapayuka huku wakitikisa makoti yao na kurusha vumbi angani. Mkuu wa jeshi aliwaamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome, akawaambia wamchape viboko ili wapate kujua kisa cha Wayahudi kumpigia kelele. Lakini walipokwisha mfunga ili wamchape viboko, Paulo alimwuliza jemadari mmoja aliyesimama hapo, “Je, ni halali kwenu kumpiga viboko raia wa Roma kabla hajahukumiwa?” Yule jemadari aliposikia hayo, alimpasha habari mkuu wa jeshi akisema, “Unataka kufanya nini? Mtu huyu ni raia wa Roma!” Basi, mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamwambia, “Niambie; je, wewe ni raia wa Roma?” Paulo akamjibu, “Naam.” Mkuu wa jeshi akasema, “Mimi nami nimekuwa raia wa Roma kwa kulipa gharama kubwa.” Paulo akasema, “Lakini mimi ni raia wa Roma kwa kuzaliwa.” Wale watu ambao walikuwa tayari kumchunguza Paulo walitoweka mara. Hata yule mkuu wa jeshi aliogopa alipojua kwamba Paulo ni raia wa Roma na kwamba alikuwa amekwisha mfunga minyororo. Kesho yake, mkuu wa jeshi alitaka kujua mashtaka kamili ambayo Wayahudi walikuwa wamemwekea Paulo. Hivyo, alimfungua Paulo minyororo, akaamuru makuhani wakuu na Baraza lote wafanye kikao. Kisha alimleta Paulo, akamsimamisha mbele ya Baraza. Paulo aliwakodolea macho wale wanabaraza, halafu akaanza kusema, “Ndugu zangu, mpaka hivi leo nimekuwa nikiishi na dhamiri njema mbele ya Mungu.” Hapo kuhani mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wampige kofi mdomoni. Basi, Paulo akamwambia, “Mungu mwenyewe atakupiga kofi wewe uliye kama ukuta uliopakwa chokaa! Unawezaje kukaa hapo ili unihukumu kisheria na huku wewe mwenyewe unaivunja sheria kwa kuamuru nipigwe?” Watu waliokuwa wamesimama pale wakamwambia Paulo, “Unamtukana kuhani mkuu wa Mungu!” Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kama yeye ni kuhani mkuu. Maana Maandiko yasema hivi: ‘Usiseme vibaya juu ya mtawala wa watu wako.’” Wakati huo Paulo alikwisha tambua kwamba sehemu moja ya wanabaraza wale ilikuwa ni Masadukayo na nyingine Mafarisayo. Basi, alipaza sauti yake mbele ya Baraza, “Ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Mimi nimeletwa mahakamani kwa kuwa ninatumaini kwamba wafu watafufuka.” Baada ya kusema hivyo, mzozo mkali ulitokea kati ya Mafarisayo na Masadukayo na mkutano ukagawanyika sehemu mbili. Kisa chenyewe kilikuwa hiki, Masadukayo hushikilia kwamba wafu hawafufuki, hakuna malaika, na roho nazo hazipo. Lakini Mafarisayo husadiki hayo yote matatu. Kelele ziliongezeka na baadhi ya waalimu wa sheria wa kikundi cha Mafarisayo walisimama na kutoa malalamiko yao kwa nguvu: “Hatuoni chochote kilicho kiovu katika mtu huyu; huenda ikawa kwamba roho au malaika ameongea naye.” Mzozo ulizidi kuwa mwingi hata mkuu wa jeshi akaogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipandevipande. Kwa hiyo, aliwaamuru askari wake kuingia kati ya lile kundi, wamtoe Paulo na kumrudisha ndani ya ngome. Usiku uliofuata, Bwana alisimama karibu na Paulo, akamwambia, “Jipe moyo! Umenishuhudia hapa Yerusalemu, utafanya vivyo hivyo mjini Roma.” Kulipokucha, Wayahudi walifanya kikao cha faragha. Wakala kiapo: “Hatutakula wala kunywa mpaka tutakapokuwa tumekwisha muua Paulo.” Watu zaidi ya arubaini ndio waliokula njama kufanya hivyo. Basi, walikwenda kwa makuhani wakuu na wazee, wakasema, “Sisi tumekula kiapo kwamba hatutaonja chochote kwa vinywa vyetu mpaka hapo tutakapokuwa tumemuua Paulo. Sasa basi, nyinyi pamoja na Baraza tumeni ujumbe kwa mkuu wa jeshi ili amlete Paulo kwenu mkijisingizia kwamba mnataka kupata habari kamili zaidi juu yake. Tuko tayari kumwua hata kabla hajafika karibu.” Lakini mtoto wa ndugu yake Paulo alisikia juu ya mpango huo; hivyo akaenda ndani ya ngome, akamjulisha Paulo juu ya njama hiyo. Hapo Paulo akamwita mmoja wa maaskari, akamwambia, “Mchukue kijana huyu kwa mkuu wa jeshi; ana kitu cha kumwambia.” Askari akamchukua huyo kijana, akamwongoza mpaka kwa mkuu wa jeshi, akasema, “Yule mfungwa Paulo ameniita akaniomba nimlete kijana huyu kwako kwa maana ana jambo la kukuambia.” Mkuu wa jeshi alimshika huyo kijana mkono, akampeleka mahali pa faragha, akamwuliza, “Una nini cha kuniambia?” Yeye akasema, “Wayahudi wamepatana wakuombe umpeleke Paulo Barazani wakijisingizia kwamba Baraza lingependa kupata habari kamili zaidi juu yake. Lakini wewe usikubali kwa maana kuna watu zaidi ya arubaini walio tayari kumvamia. Wameapa kutokula wala kunywa kitu mpaka watakapokuwa wamemuua. Sasa wako tayari, wanangojea tu uamuzi wako.” Mkuu wa jeshi alimwacha aende zake akimwonya asimwambie mtu yeyote kwamba amemletea habari hizo. Basi, mkuu wa jeshi aliwaita askari wawili akawaambia, “Wekeni tayari askari 200, wapandafarasi sabini na askari 200 wa mikuki, waende Kaisarea; muwe tayari kuondoka kabla ya saa tatu leo usiku. Wekeni farasi kadhaa kwa ajili ya Paulo; mfikisheni salama kwa Felisi, mkuu wa mkoa.” Halafu mkuu huyo wa jeshi akaandika barua hivi: “Mimi Klaudio Lusia ninakuandikia wewe Mheshimiwa Felisi, mkuu wa mkoa. Salamu! “Wayahudi walimkamata mtu huyu na karibu wangemuua kama nisingalifahamishwa kwamba yeye ni raia wa Roma na hivyo nikaenda pamoja na askari nikamwokoa. Nilimpeleka mbele ya Baraza lao kuu nikitaka kujua kisa cha mashtaka yao. Niligundua kwamba mashtaka yenyewe yalihusu ubishi juu ya sehemu kadha wa kadha za sheria yao na hivyo sikuona kwamba amefanya chochote kinachostahili auawe au afungwe gerezani. Nilipofahamishwa kwamba Wayahudi walikuwa wamefanya njama za kumwua, niliamua kumleta kwako, nikawaambia washtaki wake walete mashtaka yao mbele yako.” Basi, hao askari walimchukua Paulo kama walivyoamriwa; wakampeleka usiku uleule mpaka Antipatri. Kesho yake askari wa miguu walirudi ngomeni, wakawaacha wale askari wapandafarasi waendelee na safari pamoja na Paulo. Walipofika Kaisarea walimpa mkuu wa mkoa ile barua na kumweka Paulo chini ya mamlaka yake. Felisi alipoisoma hiyo barua aliwauliza Paulo ametoka mkoa gani. Alipofahamishwa kwamba alikuwa ametoka mkoa wa Kilikia, akasema, “Nitasikiliza kesi yako baada ya washtaki wako kufika.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi ndani ya ukumbi wa Herode. Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania aliwasili Kaisarea pamoja na wazee kadhaa na wakili mmoja wa sheria aitwaye Tertulo. Walimwendea yule mkuu wa mkoa wakamweleza mashtaka yao juu ya Paulo. Paulo aliitwa, na Tertulo akafungua mashtaka hivi: “Mheshimiwa Felisi, uongozi wako bora umeleta amani kubwa na marekebisho ya lazima yanafanywa kwa manufaa ya taifa letu. Tunalipokea jambo hili kwa furaha daima na kutoa shukrani nyingi kwako kila mahali. Lakini, bila kupoteza wakati wako zaidi, tunakusihi kwa wema wako, usikilize taarifa yetu fupi. Tumegundua kwamba mtu huyu ni wa hatari mno. Yeye huanzisha ghasia kati ya Wayahudi kila mahali duniani na pia ni kiongozi wa kile chama cha Wanazareti. Tena alijaribu kulikufuru hekalu, nasi tukamtia nguvuni. [Tulitaka kumhukumu kufuatana na sheria yetu. Lakini Lusia, mkuu wa jeshi, aliingilia kati, akamchukua kwa nguvu kutoka mikononi mwetu. Kisha akaamuru washtaki wake waje mbele yako.] Kama ukimhoji wewe mwenyewe, utaweza kubainisha mambo haya yote tunayomshtaki kwayo.” Nao Wayahudi waliunga mkono mashtaka hayo wakisema kwamba hayo yote yalikuwa kweli. Basi, mkuu wa mkoa alimwashiria Paulo aseme. Naye Paulo akasema, “Nafurahi kujitetea mbele yako nikijua kwamba umekuwa hakimu wa taifa hili kwa miaka mingi. Unaweza kujihakikishia kwamba si zaidi ya siku kumi na mbili tu zimepita tangu nilipokwenda kuabudu Yerusalemu. Wayahudi hawakunikuta nikijadiliana na mtu yeyote. Hawakunikuta nikichochea watu hekaluni, wala katika masunagogi yao, wala mahali pengine popote katika mji huo. Wala hawawezi kuthibitisha mashtaka waliyotoa juu yangu. Ninachokubali mbele yako ni hiki: Mimi ninamwabudu Mungu wa wazee wetu nikiishi kufuatana na njia ile ambayo wao wanaiita chama cha uzushi. Ninaamini mambo yote yaliyoandikwa katika vitabu vya sheria na manabii. Mimi namtumainia Mungu, na wao wanalo tumaini hilo, kwamba watu, wema na wabaya, watafufuka. Kwa hiyo ninajitahidi daima kuwa na dhamiri njema mbele ya Mungu na mbele ya watu. “Baada ya kukaa mbali kwa miaka kadhaa, nilirudi Yerusalemu ili kuwapelekea wananchi wenzangu msaada na kutoa tambiko. Wakati nilipokuwa nikifanya hayo ndipo waliponikuta hekaluni, nilipokuwa nimekwisha fanya ile ibada ya kujitakasa. Hakukuwako kundi la watu wala ghasia. Lakini kulikuwa na Wayahudi wengine kutoka mkoa wa Asia; hao ndio wangepaswa kuwa hapa mbele yako na kutoa mashtaka yao kama wana chochote cha kusema dhidi yangu. Au, waache hawa walio hapa waseme kosa waliloliona kwangu wakati niliposimama mbele ya Baraza lao kuu, isipokuwa tu maneno haya niliyosema niliposimama mbele yao: ‘Mnanihukumu leo hii kwa sababu ya kushikilia kwamba wafu watafufuliwa!’” Hapo, Felisi, ambaye mwenyewe alikuwa anaifahamu hiyo njia vizuri, aliahirisha kesi hiyo. Akawaambia, “Nitatoa hukumu juu ya kesi hiyo wakati Lusia, mkuu wa jeshi, atakapokuja hapa.” Kisha akamwamuru yule jemadari amweke Paulo kizuizini, lakini awe na uhuru kiasi, na rafiki zake wasizuiwe kumpatia mahitaji yake. Baada ya siku chache, Felisi alifika pamoja na mkewe Drusila ambaye alikuwa Myahudi. Aliamuru Paulo aletwe, akamsikiliza akiongea juu ya kumwamini Yesu Kristo. Lakini wakati Paulo alipoanza kuongea juu ya uadilifu, juu ya kuwa na kiasi na juu ya siku ya hukumu inayokuja, Felisi aliogopa, akasema, “Kwa sasa unaweza kwenda; nitakuita tena nitakapopata nafasi.” Wakati huohuo alikuwa anatumaini kwamba Paulo angempa fedha. Kwa sababu hii alimwita Paulo mara kwa mara na kuzungumza naye. Baada ya miaka miwili, Porkio Festo alichukua nafasi ya Felisi, akawa mkuu wa mkoa. Kwa kuwa alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi, Felisi alimwacha Paulo kizuizini. Siku tatu baada ya kufika mkoani, Festo alitoka Kaisarea, akaenda Yerusalemu. Makuhani wakuu pamoja na viongozi wa Wayahudi walimpa habari kuhusu mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Paulo. Walimsihi Festo awafanyie fadhili kwa kumleta Paulo Yerusalemu; walikuwa wamekula njama wamuue akiwa njiani. Lakini Festo alijibu, “Paulo atabaki kizuizini kule Kaisarea na mimi nitakwenda huko karibuni. Waacheni viongozi wenu waende huko pamoja nami wakatoe mashtaka yao juu yake kama amefanya chochote kiovu.” Festo alikaa nao kwa muda wa siku nane au kumi hivi, kisha akarudi Kaisarea. Kesho yake alikwenda barazani, akaamuru Paulo aletwe ndani. Wakati Paulo alipofika, Wayahudi waliokuwa wametoka Yerusalemu walimzunguka wakaanza kutoa mashtaka mengi mazitomazito ambayo hawakuweza kuthibitisha. Kwa kujitetea, Paulo alisema, “Mimi sikufanya kosa lolote kuhusu sheria ya Wayahudi, wala kuhusu hekalu, wala kumhusu Kaisari.” Festo alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi na hivyo akamwuliza Paulo, “Je, ungependa kwenda Yerusalemu na huko ukahukumiwe mbele yangu kuhusu mashtaka haya?” Paulo akajibu, “Nasimama mbele ya mahakama ya Kaisari, na papa hapa ndipo ninapopaswa kupewa hukumu. Kama unavyojua vizuri, sikuwatendea Wayahudi ubaya wowote. Basi, ikiwa nimepatikana na kosa linalostahili adhabu ya kifo, siombi kusamehewa adhabu hiyo. Lakini kama hakuna ukweli katika mashtaka waliyotoa watu hawa, hakuna awezaye kunikabidhi kwao. Nakata rufani kwa Kaisari!” Basi, baada ya Festo kuzungumza na washauri wake, akamwambia Paulo, “Umekata rufani kwa Kaisari, basi, utakwenda kwa Kaisari.” Siku chache baadaye, mfalme Agripa na Bernike walifika Kaisarea ili kutoa heshima zao kwa Festo. Walikuwa huko siku kadhaa naye Festo akamweleza mfalme kesi ya Paulo: “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Felisi alimwacha kizuizini. Nilipokwenda Yerusalemu makuhani wakuu na wazee wa Wayahudi walimshtaki na kuniomba nimhukumu. Lakini mimi niliwajibu kwamba si desturi ya Waroma kumtoa mtu aadhibiwe kabla mshtakiwa hajakutana na washtaki wake ana kwa ana na kupewa fursa ya kujitetea kuhusu hayo mashtaka. Basi, walipofika hapa sikukawia, ila nilifanya kikao mahakamani kesho yake, nikaamuru mtu huyo aletwe. Washtaki wake walisimama lakini hawakutoa mashtaka maovu kama nilivyokuwa ninatazamia. Ila tu walikuwa na mabishano kadhaa pamoja naye kuhusu dini yao na kuhusu mtu mmoja aitwaye Yesu ambaye alikufa, lakini Paulo anashikilia kwamba yu hai. Sikujua la kufanya kuhusu shauri hilo. Basi, nilimwuliza Paulo kama angependa kwenda mahakamani kule Yerusalemu kwa ajili ya mashtaka hayo. Lakini Paulo alikata rufani, akaomba aachwe kizuizini mpaka uamuzi wa shauri hilo ufanywe na Kaisari. Kwa hiyo niliamua akae kizuizini mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari.” Basi Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikia mtu huyo mimi mwenyewe.” Festo akamwambia, “Utamsikia kesho.” Hivyo, kesho yake, Agripa na Bernike walifika kwa shangwe katika ukumbi wa mkutano wakiwa wameandamana na wakuu wa majeshi na viongozi wa mji. Festo aliamuru Paulo aletwe ndani, kisha akasema, “Mfalme Agripa na wote mlioko hapa pamoja nasi! Hapa mbele yenu yuko mtu ambaye jumuiya yote ya Wayahudi hapa na kule Yerusalemu walinilalamikia wakipiga kelele kwamba hastahili kuishi tena. Lakini mimi sikuona kuwa alikuwa ametenda chochote kibaya hata astahili kupewa adhabu ya kifo. Lakini, kwa vile Paulo mwenyewe alikata rufani kwa Kaisari, niliamua kumpeleka. Kwa upande wangu sina habari kamili ambayo naweza kumwandikia Kaisari juu yake. Ndiyo maana nimemleta hapa mbele yenu na mbele yako mfalme Agripa, ili baada ya kumchunguza, niweze kuwa na la kuandika. Kwa maana nadhani itakuwa kichekesho kumpeleka mfungwa bila kutaja wazi mashtaka yanayomkabili.” Basi, Agripa akamwambia Paulo, “Unaruhusiwa kujitetea.” Hapo Paulo alinyosha mkono wake akajitetea hivi: “Mfalme Agripa, ninajiona mwenye bahati leo kujitetea mbele yako kuhusu yale mashtaka yote ambayo Wayahudi walikuwa wamesema juu yangu. Hasa kwa vile wewe mwenyewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na migogoro yao, ninakuomba basi unisikilize kwa uvumilivu. “Wayahudi wanajua habari za maisha yangu tangu utoto, jinsi nilivyoishi tangu mwanzo kati ya taifa langu huko Yerusalemu. Wananifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia, kama wakipenda, kwamba tangu mwanzo niliishi kama mmoja wa kikundi chenye siasa kali kabisa katika dini yetu, yaani kikundi cha Mafarisayo. Na sasa niko hapa nihukumiwe kwa sababu ninaitumainia ile ahadi ambayo Mungu aliwaahidi babu zetu. Ahadi hiyo ndiyo ileile inayotumainiwa na makabila kumi na mawili ya taifa letu, wakimtumikia Mungu kwa dhati mchana na usiku. Mheshimiwa mfalme, Wayahudi wananishtaki kwa sababu ya tumaini hilo! Kwa nini nyinyi mnaona shida sana kuamini kwamba Mungu huwafufua wafu? Kwa kweli mimi mwenyewe niliamini kwamba ni wajibu wangu kufanya mambo mengi kulipinga jina la Yesu wa Nazareti. Mambo hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Mimi binafsi, nikiwa nimepewa mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu, nilipata kuwatia gerezani wengi wa watu wa Mungu. Nao walipohukumiwa kuuawa, nilipiga kura ya kukubali. Mara nyingi niliwafanya waadhibiwe katika masunagogi yote nikiwashurutisha waikane imani yao. Hasira yangu kwao ilikuwa kubwa hata nikawasaka mpaka miji ya mbali. “Kwa mujibu huohuo, nilikwenda Damasko wakati mmoja, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu. Mheshimiwa, wakati nilipokuwa njiani, saa sita mchana, niliona mwanga mkubwa kuliko wa jua ukiangaza kutoka mbinguni, ukanizunguka mimi na wale wasafiri wenzangu. Sisi sote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikiniambia kwa Kiebrania: ‘Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa? Unajiumiza bure kama ng'ombe anayepiga teke fimbo ya bwana wake.’ Mimi nikauliza: ‘Ni nani wewe Bwana?’ Naye Bwana akajibu: ‘Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa. Haidhuru, inuka sasa; simama wima. Nimekutokea ili nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu. Utawathibitishia watu wengine mambo uliyoyaona leo na yale ambayo bado nitakuonesha. Nitakuokoa na watu wa Israeli na watu wa mataifa mengine ambao mimi ninakutuma kwao. Utayafumbua macho yao na kuwawezesha watoke gizani na kuingia katika mwanga; watoke katika utawala wa Shetani, wamgeukie Mungu; ili kwa kuamini, wapate kusamehewa dhambi na kuchukua nafasi yao kati ya wale ambao wamepata kuwa watu wa Mungu.’ “Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa maono hayo ya mbinguni. Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonesha kwa vitendo kwamba wamebadilisha mioyo yao. Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa hekaluni, wakajaribu kuniua. Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia; yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine.” Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, “Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu!” Lakini Paulo akasema, “Sina wazimu mheshimiwa Festo. Ninachosema ni ukweli mtupu. Wewe Mfalme unayafahamu mambo haya, kwa hiyo ninaweza kuongea bila woga mbele yako. Sina mashaka kwamba matukio hayo yanajulikana kwako maana jambo hili halikutendeka mafichoni. Mfalme Agripa, je, una imani na manabii? Najua kwamba unaamini.” Agripa akamjibu Paulo, “Kidogo tu utanifanya Mkristo!” Paulo akamjibu, “Namwomba Mungu kwamba, kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu bali wote wanaonisikia leo wapate kuwa kama nilivyo mimi, lakini bila hii minyororo.” Hapo mfalme Agripa, mkuu wa mkoa, Bernike na wale wote waliokuwa pamoja nao, walisimama. Walipokwisha ondoka, waliambiana, “Mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo au kifungo.” Naye Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeweza kufunguliwa kama asingalikuwa amekata rufani kwa Kaisari.” Walipokwisha amua tusafiri mpaka Italia, walimweka Paulo pamoja na wafungwa wengine chini ya ulinzi wa Yulio aliyekuwa ofisa wa jeshi katika kikosi kiitwacho “Kikosi cha Augusto.” Tulipanda meli ya Adiramito iliyokuwa inasafiri na kupitia bandari kadhaa za mkoa wa Asia, tukaanza safari. Aristarko, mwenyeji wa Makedonia kutoka Thesalonike, alikuwa pamoja nasi. Kesho yake tulitia nanga katika bandari ya Sidoni. Yulio alimtendea Paulo vizuri kwa kumruhusu awaone rafiki zake na kupata mahitaji yake. Kutoka huko tuliendelea na safari, lakini kwa kuwa upepo ulikuwa unavuma kwa kasi kutujia kwa mbele, tulipitia upande wa kisiwa cha Kupro ambapo upepo haukuwa mwingi. Halafu tulivuka bahari ya Kilikia na Pamfulia, tukatia nanga Mura, mji wa Lukia. Hapo yule ofisa alikuta meli moja ya Aleksandria iliyokuwa inakwenda Italia, na hivyo akatupandisha ndani. Kwa muda wa siku nyingi tulisafiri polepole, na kwa shida tulifika karibu na Nido. Kwa sababu upepo ulikuwa bado unatupinga, tuliendelea mbele moja kwa moja tukapitia upande wa Krete karibu na rasi Salmone ambapo upepo haukuwa mwingi. Tulipita kando yake polepole tukafika mahali paitwapo “Bandari Nzuri,” karibu na mji wa Lasea. Muda mrefu ulikuwa umepita, na hata siku ya kufunga ilikuwa imekwisha pita. Sasa ilikuwa hatari sana kusafiri kwa meli. Basi, Paulo aliwapa onyo: “Waheshimiwa, nahisi kwamba safari hii itakuwa ya shida na hasara nyingi si kwa shehena na meli tu, bali pia kwa maisha yetu.” Lakini yule ofisa alivutiwa zaidi na maoni ya nahodha na ya mwenye meli kuliko yale aliyosema Paulo. Kwa kuwa bandari hiyo haikuwa mahali pazuri pa kukaa wakati wa baridi, wengi walipendelea kuendelea na safari, ikiwezekana mpaka Foinike. Foinike ni bandari ya Krete inayoelekea kusini-magharibi na kaskazini-magharibi; na huko wangeweza kukaa wakati wa baridi. Basi, upepo mzuri wa kusi ulianza kuvuma, nao wakadhani wamefanikiwa lengo lao; hivyo wakangoa nanga, wakaiendesha meli karibu sana na pwani ya Krete. Lakini haukupita muda, upepo mkali uitwao “Upepo wa Kaskazi” ulianza kuvuma kutoka kisiwani. Upepo uliipiga ile meli, na kwa kuwa hatukuweza kuukabili, tukaiacha ikokotwe na huo upepo. Kisiwa kimoja kiitwacho Kauda kilitukinga kidogo na ule upepo; na tulipopita kusini mwake tulifaulu, ingawa kwa shida, kuusalimisha ule mtumbwi wa meli. Wale wanamaji waliuvuta mtumbwi ndani, kisha wakaizungushia meli kamba na kuifunga kwa nguvu. Waliogopa kwamba wangeweza kukwama kwenye ufuko wa bahari, pwani ya Libia. Kwa hiyo walishusha matanga na kuiacha meli ikokotwe na upepo. Dhoruba iliendelea kuvuma na kesho yake wakaanza kutupa nje shehena ya meli. Siku ya tatu, wakaanza pia kutupa majini vifaa vya meli kwa mikono yao wenyewe. Kwa muda wa siku nyingi hatukuweza kuona jua wala nyota; dhoruba iliendelea kuvuma sana, hata matumaini yote ya kuokoka yakatuishia. Baada ya kukaa muda mrefu bila kula chakula, Paulo alisimama kati yao, akasema, “Waheshimiwa, ingalikuwa afadhali kama mngalinisikiliza na kuacha kusafiri kutoka Krete. Kama mngalifanya hivyo tungaliiepuka shida hii na hasara hizi zote. Lakini sasa ninawaombeni muwe na moyo; hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake; meli tu ndiyo itakayopotea. Kwa maana jana usiku malaika wa yule Mungu ambaye mimi ni wake na ambaye mimi ninamwabudu alinitokea, akaniambia: ‘Paulo, usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari; naye Mungu, kwa wema wake, amekufadhili kwa kuwaokoa wote wanaosafiri nawe wasiangamie.’ Hivyo, waheshimiwa, jipeni moyo! Maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa sawa kama nilivyoambiwa. Lakini ni lazima tutatupwa ufukoni mwa kisiwa fulani.” Usiku wa siku ya kumi na nne, tulikuwa tunakokotwa huku na huko katika bahari ya Adria. Karibu na usiku wa manane wanamaji walijihisi kuwa karibu na nchi kavu. Hivyo walitafuta kina cha bahari kwa kuteremsha kamba iliyokuwa imefungiwa kitu kizito, wakapata kina cha mita arubaini. Baadaye wakapima tena wakapata mita thelathini. Kwa sababu ya kuogopa kukwama kwenye miamba, waliteremsha nanga nne nyuma ya meli; wakaomba kuche upesi. Wanamaji walitaka kutoroka, na walikwisha kuteremsha ule mtumbwi majini, wakijisingizia kwamba wanakwenda kuteremsha nanga upande wa mbele wa meli. Lakini Paulo alimwambia yule ofisa wa jeshi na askari wake, “Kama wanamaji hawa hawabaki ndani ya meli, hamtaokoka.” Hapo wale askari walizikata kamba zilizokuwa zimeshikilia ule mtumbwi, wakauacha uchukuliwe na maji. Karibu na alfajiri, Paulo aliwahimiza wote wale chakula: “Kwa siku kumi na nne sasa mmekuwa katika mashaka na bila kula; hamjala kitu chochote. Basi, ninawasihi mle chakula kwa maana mnakihitaji ili mweze kuendelea kuishi. Maana hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea.” Baada ya kusema hivyo, Paulo alichukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega, akaanza kula. Hapo wote wakapata moyo, nao pia wakala chakula. Jumla tulikuwa watu 276 katika meli. Baada ya kila mmoja kula chakula cha kutosha, walipunguza uzito wa meli kwa kutupa nafaka baharini. Kulipokucha, wanamaji hawakuweza kuitambua nchi ile, ila waliona ghuba moja yenye ufuko; wakaamua kutia nanga huko kama ikiwezekana. Hivyo walikata nanga na kuziacha baharini, na wakati huohuo wakazifungua kamba zilizokuwa zimeufunga usukani, kisha wakatweka tanga moja mbele kushika upepo, wakaelekea ufukoni. Lakini walifika mahali ambapo mikondo miwili ya bahari hukutana, na meli ikakwama. Sehemu ya mbele ilikuwa imezama mchangani bila kutikisika. Sehemu ya nyuma ya meli ilianza kuvunjika vipandevipande kwa mapigo ya nguvu ya mawimbi. Askari walitaka kuwaua wafungwa wote kwa kuogopa kwamba wangeogelea hadi pwani na kutoroka. Lakini kwa vile yule ofisajeshi alitaka kumwokoa Paulo, aliwazuia wasifanye hivyo. Aliamuru wale waliojua kuogelea waruke kutoka melini na kuogelea hadi pwani, na wengine wafuate wakijishikilia kwenye mbao au kwenye vipande vya meli iliyovunjika. Ndivyo sisi sote tulivyofika salama pwani. Tulipokwisha fika salama kwenye nchi kavu, tuligundua kwamba kile kisiwa kinaitwa Malta. Wenyeji wa hapo walikuwa wema sana kwetu. Mvua ilikuwa inaanza kunyesha na kulikuwa na baridi, hivyo waliwasha moto, wakatukaribisha. Paulo aliokota mzigo mdogo wa kuni akawa anazitia motoni. Hapo, kwa sababu ya lile joto la moto, nyoka akatoka katika kuni akamnasa Paulo mkononi na kujishikilia hapo. Wenyeji wa pale walipokiona kile kiumbe kinaninginia kwenye mkono wake waliambiana, “Bila shaka mtu huyu amekwisha ua mtu, na ingawa ameokoka kuangamia baharini, ‘Haki’ haitamwacha aendelee kuishi!” Lakini Paulo alikikungutia kile kiumbe motoni na hakuumizwa hata kidogo. Wale watu walikuwa wakitazamia kwamba angevimba au angeanguka chini na kufa ghafla. Baada ya kungojea kwa muda mrefu bila kuona kwamba Paulo amepatwa na jambo lolote lisilo la kawaida, walibadilisha fikira zao juu yake, wakasema kuwa yeye ni mungu. Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya Publio, mkuu wa kile kisiwa. Publio alitukaribisha kirafiki, tukawa wageni wake kwa siku tatu. Basi, ikawa kwamba baba yake Publio alikuwa amelala kitandani, mgonjwa wa homa na kuhara. Paulo alikwenda kumwona na baada ya kusali, akaweka mikono yake juu ya mgonjwa, akamponya. Kutokana na tukio hilo, wagonjwa wote katika kile kisiwa walikuja wakaponywa. Watu walitupatia zawadi mbalimbali na wakati tulipoanza tena safari, walitia ndani ya meli masurufu tuliyohitaji. Baada ya miezi mitatu tulianza tena safari yetu kwa meli moja ya Aleksandria iitwayo “Miungu Pacha”. Meli hiyo ilikuwa imetia nanga kisiwani wakati wote wa baridi. Tulifika katika mji wa Sirakusa, tukakaa hapo kwa siku tatu. Toka huko tulingoa nanga, tukazunguka na kufika Regio. Baada ya siku moja, upepo ulianza kuvuma kutoka kusini, na baada ya siku mbili tulifika bandari ya Potioli. Huko tuliwakuta ndugu kadhaa ambao walituomba tukae nao kwa juma moja. Hivi ndivyo tulivyopata kufika Roma. Ndugu wa kule Roma walipopata habari zetu, wakaja kutulaki kwenye soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akapata moyo. Tulipofika Roma, Paulo aliruhusiwa kukaa peke yake pamoja na askari mmoja wa kumlinda. Baada ya siku tatu, Paulo aliwaita pamoja viongozi wa Kiyahudi wa mahali hapo. Walipokusanyika, Paulo aliwaambia, “Wananchi wenzangu, mimi, ingawa sikufanya chochote kibaya wala kupinga desturi za wazee wetu, nilitiwa nguvuni kule Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa Waroma. Waliponihoji na kuona kwamba sikuwa na hatia yoyote, walitaka kuniachia. Lakini Wayahudi wengine walipinga jambo hilo, nami nikalazimika kukata rufani kwa Kaisari, ingawa sikuwa na chochote cha kuwashtaki wananchi wenzangu. Ni kwa sababu hiyo nimeomba kuonana na kuongea nanyi, maana nimefungwa minyororo hii kwa sababu ya tumaini lile la Israeli.” Wao wakamwambia, “Sisi hatujapokea barua yoyote kutoka Yudea, wala hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa na kutoa habari rasmi au kusema chochote kibaya juu yako. Lakini tunafikiri inafaa tusikie kutoka kwako mwenyewe mambo yaliyo kichwani mwako. Kwa maana tujualo sisi kuhusu hicho kikundi ni kwamba kinapingwa kila mahali.” Basi, walipanga naye siku kamili ya kukutana, na wengi wakafika huko alikokuwa anakaa. Tangu asubuhi mpaka jioni Paulo aliwaeleza na kuwafafanulia juu ya ufalme wa Mungu, akijaribu kuwafanya wakubali habari juu ya Yesu kwa kutumia sheria na maandiko ya manabii. Baadhi yao walikubali maneno yake, lakini wengine hawakuamini. Basi, kukawa na mtengano wa fikira kati yao. Walipokuwa wanakwenda zao, Paulo alisema jambo hili: “Kweli ni sawa yale Roho Mtakatifu aliyowaarifu wazee wenu kwa njia ya nabii Isaya akisema: ‘Nenda kwa watu hawa ukawaambie: Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa; kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameziba masikio yao, wamefumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao. Wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.’” Halafu Paulo akasema, “Jueni basi, kwamba ujumbe wa Mungu juu ya wokovu umepelekwa kwa watu wa mataifa. Wao watasikiliza!” [ Paulo alipokwisha sema hayo, Wayahudi walijiondokea huku wakiwa wanabishana vikali wao kwa wao.] Kwa muda wa miaka miwili mizima Paulo aliishi katika nyumba aliyoipanga yeye mwenyewe; akawa anawakaribisha wote waliofika kumsalimu. Alikuwa akihubiri ufalme wa Mungu na kufundisha juu ya Bwana Yesu Kristo kwa uhodari, bila kizuizi. Kutoka kwangu mimi Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, na mtume niliyeteuliwa na kuitwa kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema ya Mungu. Hapo kale, Mungu aliwaahidi watu hii Habari Njema kwa njia ya manabii wake katika Maandiko Matakatifu. Hii Habari Njema inamhusu Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kuhusu ubinadamu wake, alikuwa mzawa wa Daudi; kuhusu utakatifu wake wa kimungu, alithibitishwa kwa uwezo mkuu kwamba ni Mwana wa Mungu kwa kufufuliwa kutoka kwa wafu. Kwa njia yake, mimi nimepewa neema ya kuwa mtume, ili kwa ajili yake niwaongoze watu wa mataifa yote wapate kuamini na kutii. Nyinyi ni miongoni mwa watu hao; mmeitwa muwe watu wake Yesu Kristo. Basi, nawaandikia nyinyi nyote mlioko Roma ambao Mungu anawapenda, akawateua muwe watu wake. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo. Awali ya yote, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inasikika duniani kote. Mungu, ambaye ninamtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Habari Njema ya Mwanae, ni shahidi wangu kwamba ninawakumbukeni daima katika sala zangu. Namwomba Mungu akipenda, anipatie nafasi nzuri ya kuja kwenu sasa. Kwa maana ninatamani sana kuwaoneni ili nipate kuwagawieni zawadi ya kiroho na kuwaimarisha. Ndiyo kusema, tutaimarishana: Imani yenu itaniimarisha mimi, na yangu itawaimarisha nyinyi. Ndugu zangu, nataka mjue kwamba mara nyingi nilikusudia kuwatembeleeni, lakini mpaka sasa nimezuiwa. Ningependa kupata mafanikio mema kati yenu kama nilivyopata kati ya watu wa mataifa mengine. Ninalo jukumu kwa watu wote, waliostaarabika na wasiostaarabika, wenye elimu na wasio na elimu. Ndiyo maana ninatamani pia kuihubiri Habari Njema kwenu nyinyi mlioko huko Roma. Sioni aibu kutangaza Habari Njema; yenyewe ni nguvu ya Mungu inayowaokoa wote wanaoamini: Wayahudi kwanza na wasio Wayahudi pia. Kwa maana Habari Njema inaonesha wazi jinsi Mungu anavyowakubali watu kuwa waadilifu; jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho; kama ilivyoandikwa: “Mwadilifu kwa imani ataishi.” Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi na uovu wote wa binadamu ambao kwa njia zao mbaya wanaupinga ukweli usijulikane. Kwa maana, yote yanayoweza kujulikana juu ya Mungu ni wazi kwao; maana Mungu mwenyewe ameyadhihirisha. Tangu Mungu alipoumba ulimwengu, uwezo wake wa milele na uungu wake, ingawa havionekani kwa macho, vinafahamika wazi. Watu wanaweza kuyajua mambo hayo kutokana na vitu hivyo alivyoumba Mungu. Kwa hiyo hawana njia yoyote ya kujitetea! Ingawa wanajua kuna Mungu, lakini hawampi heshima anayostahili, wala hawamshukuru. Badala yake, fikira zao zimekuwa batili na akili zao tupu zimejaa giza. Wanajidai kuwa wenye hekima, kumbe ni wapumbavu. Wanaacha kumwabudu Mungu aishiye milele, na badala yake, wanaabudu sanamu zilizo mfano wa binadamu ambaye hufa, mfano wa wanyama, ndege, au wanyama watambaao. Kwa sababu hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya za mioyo yao na kufanyiana mambo ya aibu kwa miili yao. Wanaubadili ukweli juu ya Mungu kwa uongo; wanaheshimu na kuabudu kiumbe badala ya Muumba mwenyewe, ambaye ndiye astahiliye sifa milele! Amina. Kwa hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya. Hata wanawake wanabadili matumizi yanayopatana na maumbile. Nao wanaume hali kadhalika, wanaacha kufuata matumizi ya maumbile ya mume na mke, wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wanafanyiana mambo ya aibu, na hivyo wanajiletea wenyewe adhabu wanayostahili kwa vitendo vyao viovu. Kwa vile watu walikataa kumtambua Mungu, Mungu amewaacha katika fikira zao potovu, wakafanya yale ambayo hawangestahili kufanya. Wamejaa kila aina ya uovu, dhuluma, ulafi na ufisadi. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu na nia mbaya; husengenya, na kusingiziana; ni watu wa kuchukiza kwa Mungu, wafidhuli, wenye kiburi na majivuno; hodari sana katika kutenda mabaya, na hawawatii wazazi wao; hawana dhamiri, hawatimizi ahadi zao, hawana wema wala huruma kwa wengine. Wanajua kwamba sheria ya Mungu yasema kwamba watu wanaoishi mithili hiyo, wanastahili kifo. Zaidi ya hayo, siyo tu kwamba wanafanya mambo hayo wao wenyewe, bali hata huwapongeza wale wanaofanya mambo hayohayo. Basi, rafiki, kama unawahukumu wengine, huwezi kamwe kujitetea, hata kama wewe ni nani. Kwa maana, kwa kuwahukumu wengine, unajilaani wewe mwenyewe kwa vile nawe unayafanya mambo yaleyale unayohukumu. Tunajua kwamba hukumu ya Mungu kwa wale wanaofanya mambo kama hayo ni hukumu ya haki. Lakini wewe rafiki unayewahukumu wale wanaofanya mambo kama hayo hali wewe pia unayafanya, je unadhani utaiepa hukumu ya Mungu? Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu? Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajirundikia adhabu kwa siku ile ya ghadhabu wakati hukumu ya haki ya Mungu itakapodhihirishwa. Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake. Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uhai wa milele. Lakini wale wengine wenye ubinafsi, wenye kukataa mambo ya haki na kufuata uovu, wataangukiwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. Mateso na maumivu yatampata binadamu yeyote atendaye uovu. Yatawapata Wayahudi kwanza na watu wa mataifa mengine pia. Lakini Mungu atawapa utukufu, heshima na amani wale wanaotenda mema; Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia. Maana Mungu hambagui mtu yeyote. Wale wanaotenda dhambi bila kuijua sheria wataangamia ingawaje hawaijui sheria. Na wale wanaotenda dhambi wakiwa wanaijua sheria watahukumiwa kisheria. Maana sio wanaosikia sheria ndio walio waadilifu mbele ya Mungu, ila wenye kuitii sheria ndio watakaokubaliwa kuwa waadilifu. Mathalani: Watu wa mataifa mengine hawana sheria; lakini kila wanapotimiza matakwa ya sheria wakiongozwa na dhamiri zao, wao wenyewe wanakuwa kipimo cha sheria ingawa hawaijui sheria. Mwenendo wao unaonesha kwamba matakwa ya sheria yameandikwa mioyoni mwao. Dhamiri zao zinashuhudia pia jambo hilo, maana fikira zao mara nyingine huwashtaki, na mara nyingine huwatetea. Hivyo, kufuatana na hii Habari Njema ninayohubiri, ndivyo itakavyokuwa wakati Mungu atakapohukumu mambo ya siri ya binadamu kwa njia ya Yesu Kristo. Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia sheria na kujivunia kuwa wa Mungu; kwa njia ya sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema; wewe unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani; unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo katika sheria picha kamili ya elimu na ukweli. Basi, wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba. Unasema: “Msizini,” na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu. Kwa kujigamba ati unayo sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja sheria unamdharau Mungu? Kama vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Watu wa mataifa mengine wamelikufuru jina la Mungu kwa sababu yenu nyinyi Wayahudi!” Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii sheria. Lakini kama unaivunja sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa. Kama mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya sheria, hakika atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa. Watu wa mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja sheria, ingawaje unayo maandishi ya sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii sheria ingawa hawakutahiriwa. Ndiyo kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili. Myahudi wa kweli ni yule aliye Myahudi kwa ndani, yaani yule ambaye ametahiriwa moyoni. Hili ni jambo la Roho, na si jambo la maandishi ya sheria. Mtu wa namna hiyo anapata sifa, si kutoka kwa watu, bali kutoka kwa Mungu. Basi, Myahudi ana nini zaidi kuliko watu wengine? Au kutahiriwa kuna faida gani? Naam, iko faida kwa kila upande. Kwanza, Mungu aliwakabidhi Wayahudi ujumbe wake. Lakini itakuwaje iwapo baadhi yao hawakuwa waaminifu? Je, jambo hilo litaondoa uaminifu wa Mungu? Hata kidogo! Mungu hubaki mwaminifu daima, ingawaje kila binadamu ni mwongo. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kila usemapo, maneno yako ni ya kweli; na katika hukumu, wewe hushinda.” Lakini, ikiwa uovu wetu unathibitisha kwamba Mungu anatenda kwa haki, tutasema nini? Je, tutasema kwamba anakosa haki akituadhibu? (Hapa naongea kibinadamu). Hata kidogo! Ingekuwa hivyo, Mungu angewezaje kuuhukumu ulimwengu? Labda utasema: “Ikiwa ukosefu wa uaminifu kwa upande wangu unamdhihirisha Mungu kuwa mwaminifu zaidi na hivyo kumpatia utukufu, basi singepaswa kuhukumiwa kuwa mwenye dhambi!” Ni sawa na kusema: Tufanye maovu ili tupate mema! Ndivyo wengine walivyotukashifu kwa kutushtaki kwamba tumefundisha hivyo. Watahukumiwa wanavyostahili! Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora kuliko wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu! Hakuna mtu anayeelewa, wala anayemtafuta Mungu. Wote wamepotoka wote wamekosa; hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja. Makoo yao ni kama kaburi wazi, ndimi zao zimejaa udanganyifu, midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka. Vinywa vyao vimejaa laana chungu. Miguu yao iko mbioni kumwaga damu, popote waendapo husababisha maafa na mateso; njia ya amani hawaijui. Hawajali kabisa kumcha Mungu.” Tunajua kwamba sheria huwahusu walio chini ya sheria hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu. Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kushika sheria; kazi ya sheria ni kumwonesha tu mtu kwamba ametenda dhambi. Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea sheria. Sheria na manabii hushuhudia jambo hili. Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote. Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu. Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa. Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate kuonesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila kuzijali dhambi za watu; sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu apate kuonesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonesha kwamba yeye ni mwadilifu na kwamba humfanya kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini Yesu. Basi, tunaweza kujivunia nini? Hakuna! Kwa nini? Je, kwa sababu ya kutimiza sheria? La! Bali kwa sababu tunaamini. Maana Mungu humkubali mtu kuwa mwadilifu kwa imani, wala si kwa kutimiza matakwa ya sheria. Au je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu, ama pia wa watu wa mataifa mengine? Naam, wa watu wa mataifa mengine pia. Mungu ni mmoja, naye atawafanya Wayahudi kuwa waadilifu kwa imani yao, na watu wa mataifa mengine pia kwa imani yao. Je, tunaitumia imani kuibatilisha sheria? Hata kidogo; bali tunaipa sheria thamani yake kamili. Tuseme nini basi, juu ya Abrahamu baba yetu? Kama Abrahamu alikuwa amefanywa mwadilifu kutokana na bidii yake, basi, anacho kitu cha kujivunia mbele ya Mungu. Kwa maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Abrahamu alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.” Mfanyakazi hulipwa mshahara; mshahara wake si zawadi bali ni haki yake. Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu, basi, Mungu huijali imani ya mtu huyo, akamkubali kuwa mwadilifu. Naye Daudi asema hivi juu ya furaha ya mtu yule ambaye Mungu amemkubali kuwa mwadilifu bila kuyajali matendo yake: “Heri wale waliosamehewa makosa yao ambao makosa yao yamefutwa. Heri mtu yule ambaye Bwana hataziweka dhambi zake katika kumbukumbu.” Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: “Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.” Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa, ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa. Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu. Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa. Mungu alimwahidi Abrahamu na wazawa wake kwamba ulimwengu ungekuwa mali yao. Ahadi hiyo haikufanywa kwa sababu Abrahamu aliitii sheria, bali kwa kuwa aliamini, akakubaliwa kuwa mwadilifu. Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu wanaoitii sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu. Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna sheria, haiwezekani kuivunja. Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi hiyo ni kwa ajili ya wote: Si kwa wale tu wanaoishika sheria, bali pia kwa wale waishio kwa imani kama Abrahamu. Yeye ni baba yetu sisi sote. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.” Ahadi hiyo ni kweli mbele ya Mungu ambaye Abrahamu alimwamini-Mungu ambaye huwapa wafu uhai, na kwa amri yake, vitu ambavyo havikuwapo huwa. Abrahamu aliamini na kutumaini ingawa hali yenyewe ilikuwa bila matumaini, na hivyo amekuwa baba wa mataifa mengi kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Wazawa wako watakuwa wengi kama nyota!” Alikuwa mzee wa karibu miaka 100, lakini imani yake haikufifia ingawa alijua kwamba mwili wake ulikuwa kama umekufa, na pia mkewe, Sara, alikuwa tasa. Abrahamu hakuionea mashaka ile ahadi ya Mungu; alipata nguvu kutokana na imani, akamtukuza Mungu. Alijua kwamba Mungu anaweza kuyatekeleza yale aliyoahidi. Ndiyo maana Mungu alimkubali kuwa mwadilifu. Inaposemwa, “Alimkubali,” haisemwi kwa ajili yake mwenyewe tu. Jambo hili linatuhusu sisi pia ambao tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, kutoka kwa wafu. Yeye alitolewa auawe kwa ajili ya dhambi zetu, akafufuka ili tufanywe waadilifu. Sasa, kwa vile tumefanywa kuwa waadilifu kwa imani, basi tunayo amani naye Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa imani yetu, yeye ametuleta katika hali hii ya neema ya Mungu ambamo sasa tunaishi. Basi, tunajivunia tumaini tulilo nalo la kushiriki utukufu wa Mungu. Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi, nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini. Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia. Tulipokuwa bado wanyonge, Kristo, wakati ulipotimia, alikufa kwa ajili yetu sisi waovu. Si rahisi mtu kufa kwa ajili ya mtu mwadilifu; labda mtu anaweza kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu. Kwa kuwa sasa tumefanywa kuwa waadilifu kwa damu ya Kristo, ni dhahiri zaidi kwamba atatuokoa katika ghadhabu ya Mungu. Maana, tulipokuwa bado maadui zake, Mungu alitupatanisha naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa tumepatanishwa naye, ni dhahiri zaidi kwamba tutaokolewa kwa uhai wa Kristo. Wala si hayo tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ametupatanisha na Mungu. Kwa njia ya mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, nayo ikasababisha kifo. Hivyo kifo kimeenea katika jumuiya yote ya binadamu, kwa maana wote wametenda dhambi. Kabla ya sheria kuwako, dhambi ilikuwako ulimwenguni; lakini dhambi haiwekwi katika kumbukumbu bila sheria. Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Mose, kifo kiliwatawala hata wale ambao hawakutenda dhambi kama ile ya Adamu, ya kumwasi Mungu. Adamu alikuwa kielelezo cha Kristo ambaye alikuja baadaye. Lakini kosa la Adamu haliwezi kulinganishwa na neema ya Mungu. Maana, ingawa dhambi ya mtu mmoja ilisababisha kifo kwa wote, kwa fadhili ya mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, Mungu amewazidishia wote neema na zawadi zake. Kuna tofauti baina ya zawadi ya Mungu na dhambi ya mtu yule mmoja. Maana, baada ya kosa la mtu mmoja, Mungu alitoa hukumu; lakini baada ya makosa ya watu wengi, Mungu aliwapa zawadi yake kwa kuwasamehe. Kweli, kwa dhambi ya mtu mmoja, kifo kilianza kutawala kwa sababu ya huyo mtu mmoja; lakini, ni dhahiri zaidi kwamba alichokifanya yule mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, ni bora zaidi. Wote wanaopokea neema na zawadi hiyo ya kufanywa kuwa waadilifu, watatawala katika uhai kwa njia ya huyo mmoja, yaani Yesu Kristo. Basi, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta hukumu kwa binadamu wote, kadhalika kitendo kiadilifu cha mtu mmoja kinawapa wote uadilifu na uhai. Na kama kwa kutokutii kwa mtu mmoja watu wengi walifanywa wenye dhambi, kadhalika kutii kwa mtu mmoja kutawafanya wengi kuwa waadilifu. Sheria ilitokea, ikasababisha kuongezeka kwa uhalifu; lakini pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi. Kama vile dhambi ilivyotawala kwa kifo, kadhalika neema inatawala kwa uadilifu na kuleta uhai wa milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu. Tuseme nini basi? Je, tuendelee kubaki katika dhambi ili neema ya Mungu iongezeke? Hata kidogo! Kuhusu dhambi sisi tumekufa — tutaendeleaje kuishi tena katika dhambi? Maana, mnajua kwamba sisi tuliobatizwa tukaungana na Kristo Yesu, tulibatizwa na kuungana na kifo chake. Tulipobatizwa tuliungana na kifo chake, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa kitendo kitukufu cha Baba, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya. Maana, kama sisi tumeungana naye katika kufa kama yeye, vivyo hivyo tutaungana naye kwa kufufuliwa kutoka kwa wafu kama yeye. Tunajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja na Kristo, ili hali ya dhambi iharibiwe, tusiwe tena watumwa wa dhambi. Kwa maana, mtu aliyekufa, amenasuliwa kutoka dhambini. Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye. Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa kutoka kwa wafu na hafi tena; kifo hakimtawali tena. Hivyo, kwa kuwa alikufa — mara moja tu — dhambi haina nguvu tena juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu. Hali kadhalika nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Kwa hiyo, dhambi isiitawale tena miili yenu ambayo hufa, na hivyo kuzitii tamaa zake. Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni nyinyi wenyewe kwa Mungu kama watu waliofufuliwa kutoka kwa wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya uadilifu. Maana, dhambi haitawatawala tena, kwani hamko chini ya sheria, bali chini ya neema. Basi, tuseme nini? Je, tutende dhambi ati kwa sababu hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? Hata kidogo! Mnajua kwamba mkijitolea nyinyi wenyewe kama watumwa na kumtii fulani, mnakuwa kweli watumwa wake mtu huyo — au watumwa wa dhambi na matokeo yake ni kifo, au wa utii na matokeo yake ni kufanywa kuwa waadilifu. Ingawa mlikuwa watumwa wa dhambi zamani, sasa lakini — namshukuru Mungu — mmetii kwa moyo wote yale maazimio na mafundisho mliyopokea. Mlikombolewa kutoka utumwa wa dhambi, mkawa watumwa wa uadilifu (hapa natumia lugha ya kawaida ya watu kwa sababu ya udhaifu wenu wenyewe). Kama vile wakati fulani mlivyojitolea nyinyi wenyewe kutumikia uchafu na uhalifu kwa ajili ya uovu, vivyo hivyo sasa jitoleeni nafsi zenu wenyewe kutumikia uadilifu kwa ajili ya utakatifu. Mlipokuwa watumwa wa dhambi mlikuwa huru mbali na uadilifu. Sasa, mlipata faida gani siku zile kutokana na mambo yale ambayo mnayaonea aibu sasa? Maana, matokeo ya mambo haya ni kifo! Lakini sasa mmekwisha kombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mmekuwa watumishi wa Mungu; faida mliyo nayo sasa ni utakatifu, na matokeo yake ni uhai wa milele. Kwa maana mshahara wa dhambi ni kifo; lakini zawadi anayotoa Mungu ni uhai wa milele katika kuungana na Kristo Yesu, Bwana wetu. Ndugu zangu, bila shaka mtaelewa yafuatayo, maana ninawazungumzia watu wanaojua sheria. Sheria humtawala mtu wakati akiwa hai. Mathalani: Mwanamke aliyeolewa anafungwa na sheria muda wote mumewe anapokuwa hai; lakini mumewe akifa, hiyo sheria haimtawali tena huyo mwanamke. Hivyo mwanamke huyo akiishi na mwanamume mwingine wakati mumewe yungali hai, ataitwa mzinzi; lakini mumewe akifa, mwanamke huyo yu huru kisheria, na akiolewa na mwanamume mwingine, yeye si mzinzi. Hali kadhalika nyinyi ndugu zangu: Nyinyi pia mmekufa kuhusu sheria kwa kuwa nyinyi ni sehemu ya mwili wa Kristo; sasa mmekuwa wake yeye aliyefufuliwa kutoka kwa wafu ili tupate kuzaa matunda mema kwa ajili ya Mungu. Maana, tulipokuwa tukiishi kimaumbile tu, tamaa mbaya zikichochewa na sheria, zilifanya kazi katika miili yetu, na kuchuma pato la kifo. Lakini sasa tumekuwa huru kutoka vifungo vya sheria, kwa sababu tumekufa kuhusu lile jambo lililotufanya sisi watumwa. Sasa tunatumikia kufuatana na maisha mapya ya Roho, na si kufuatana na hali ile ya kale ya sheria iliyoandikwa. Je, tuseme basi, kwamba sheria ni dhambi? Hata kidogo! Lakini bila sheria, mimi nisingalijua dhambi ni kitu gani. Maana, nisingalijua ni nini hasa kutamani mabaya, kama sheria isingalikuwa imesema: “Usitamani.” Kwa kuitumia hiyo amri, dhambi ilipata fursa ya kuamsha kila aina ya tamaa mbaya ndani yangu. Maana, bila sheria dhambi ni kitu kilichokufa. Wakati mmoja mimi nilikuwa hai mbali na sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ilifufuka, nami nikafa. Hiyo amri ambayo shabaha yake ilikuwa kuleta uhai, kwangu imeleta kifo. Maana, dhambi ilichukua fursa iliyopatiwa na amri hiyo, ikanidanganya na kuniua. Basi, sheria yenyewe ni takatifu, na amri yenyewe ni takatifu, ni ya haki na nzuri. Je, hii inamaanisha kwamba kile kilicho kizuri kimesababisha kifo changu? Hata kidogo! Ilivyo ni kwamba, dhambi, ili ionekane dhahiri kuwa ni dhambi, imekitumia kile kilicho kizuri na kusababisha kifo changu. Hivyo dhambi, kwa njia ya ile amri, ilijionesha kikamilifu jinsi ilivyo mbaya mno. Tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kidunia, mimi nimeuzwa kuwa mtumwa wa dhambi. Sielewi nifanyacho, maana kile ninachotaka sikifanyi, bali kile ninachokichukia ndicho nikifanyacho. Ikiwa basi, ninatenda kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba nakubali kuwa ile sheria ni nzuri. Basi, si mimi hasa ninayefanya kitu hicho, bali ile dhambi inayokaa ndani yangu. Najua kwamba hamna jema lolote ndani yangu mimi, kadiri ya ubinadamu wangu. Kwa maana, ingawa nataka kufanya jambo jema, siwezi kulitekeleza. Yaani, badala ya kufanya lile jambo jema ninalotaka, nafanya lile baya nisilotaka. Basi, kama ninafanya kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba si mimi ninayefanya hayo, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu. Basi, nimegundua kanuni hii: Ninataka kufanya jema, lakini najikuta kwamba lile lililo baya ndilo ninalochagua. Ndani kabisa katika moyo wangu naifurahia sheria ya Mungu. Lakini naona kwamba kuna sheria nyingine inayofanya kazi mwilini mwangu, sheria ambayo inapingana na ile inayokubaliwa na akili yangu. Hiyo inanifanya niwe mtumwa wa sheria ya dhambi ifanyayo kazi mwilini mwangu. Maskini miye! Nani atakayeniokoa kutoka mwili huu unaonipeleka kifoni? Shukrani kwa Mungu afanyaye hivyo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo! Hii basi, ndiyo hali yangu: Mimi binafsi, kwa akili yangu, ninaitumikia sheria ya Mungu, lakini kwa mwili wangu ninaitumikia sheria ya dhambi. Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo. Maana, sheria ya Roho iletayo uhai kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo. Mungu ametekeleza jambo lile ambalo sheria haikuweza kutekeleza kwa sababu ya udhaifu wa binadamu. Mungu alimtuma Mwanae akiwa mwenye mwili sawa na miili yetu sisi wenye dhambi, ili aikabili dhambi, na kwa mwili huo akaiangamiza dhambi. Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho. Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho. Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uhai na amani. Maana, mwenye kutawaliwa na fikira za mwili ni adui wa Mungu; haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii. Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini nyinyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo. Lakini kama Kristo yumo ndani yenu, ingawa miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai kwa sababu mmefanywa kuwa waadilifu. Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu ataipa uhai miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu. Hivyo basi, ndugu zangu, tunalo jukumu, lakini si la kuishi kufuatana na maumbile ya kibinadamu. Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi. Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ni watoto wa Mungu. Kwa maana, hamkumpokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watumwa tena na kuwatia hofu, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watoto wa Mungu, na kwa Roho huyo, sisi tunamwita Mungu, “Aba,” yaani “Baba!” Naye Roho mwenyewe anathibitisha na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake. Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyalinganisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu. Viumbe vyote vinangojea kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake. Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini, maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto. Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukingojea tufanywe watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe. Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa. Lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona? Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu. Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka. Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu. Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake. Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Basi, wale ambao Mungu aliwateua ndio hao aliowaita; na hao aliowaita ndio hao aliowafanya kuwa waadilifu na hao aliowafanya waadilifu ndio hao aliowashirikisha pia utukufu wake. Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga? Mungu hakumhurumia hata Mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote? Ni nani atakayewashtaki wateule wa Mungu? Mungu mwenyewe huwaondolea hatia! Ni nani atakayewahukumu? Hakuna! Maana Kristo ndiye aliyekufa, tena alifufuka kutoka kwa wafu na anakaa upande wa kulia wa Mungu. Yeye anatuombea! Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha; tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa.” Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda. Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu. Nasema ukweli tupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo. Dhamiri yangu ikiongozwa na Roho Mtakatifu inanithibitishia jambo hili pia. Nataka kusema hivi: Nina huzuni kubwa na maumivu yasiyopimika moyoni mwangu kwa ajili ya ndugu zangu walio wa taifa langu! Kama ingekuwa kwa faida yao, ningekuwa radhi kulaaniwa na kutengwa na Kristo. Hao ndio watu wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu wake; alifanya nao maagano, akawapa sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake. Wao ni wajukuu wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina. Sisemi kwamba ahadi ya Mungu imebatilika; maana si watu wote wa Israeli ni wateule wa Mungu. Wala si wazawa wote wa Abrahamu ni watoto wake wa kweli. Ila, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Wazawa wake watatokana na Isaka.” Ndiyo kusema, si wale waliozaliwa kimaumbile ndio watoto wa Mungu, bali wale waliozaliwa kutokana na ahadi ya Mungu ndio watakaoitwa watoto wake. Maana ahadi yenyewe ni hii: “Wakati maalumu nitarudi, naye Sara atapata mtoto.” Tena si hayo tu, ila pia Rebeka naye alipata mapacha kwa baba mmoja, yaani Isaka, babu yetu. Lakini, ili Mungu aonekane kwamba anao uhuru wa kuchagua, hata kabla wale ndugu hawajazaliwa na kabla hawajaweza kupambanua jema na baya, Rebeka aliambiwa kwamba yule mtoto wa kwanza atamtumikia yule wa nyuma. Hivyo uchaguzi wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe, na si matendo ya binadamu. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia.” Basi, tuseme nini? Je, Mungu amekosa haki? Hata kidogo! Maana alimwambia Mose: “Nitamhurumia mtu yeyote ninayetaka kumhurumia; nitamwonea huruma mtu yeyote ninayetaka.” Kwa hiyo, yote hutegemea huruma ya Mungu, na si bidii au mapenzi ya mtu. Maana Maandiko Matakatifu yasema hivi kwa Farao: “Nilikufanya mfalme ili kwa njia yako, uwezo wangu ujulikane, na jina langu litangazwe popote duniani.” Ni wazi basi, kwamba Mungu humhurumia yeyote anayetaka kumhurumia, na akipenda kumfanya mtu awe mkaidi, hufanya hivyo. Labda utaniuliza: “Ikiwa mambo yako hivyo, Mungu anawezaje kumlaumu mtu? Nani awezaye kuyapinga mapenzi yake?” Lakini, ewe binadamu, u nani hata uthubutu kumhoji Mungu? Je, chungu chaweza kumwuliza mfinyanzi wake: “Kwa nini umenitengeneza namna hii?” Mfinyanzi anaweza kuutumia udongo apendavyo na kufinyanga vyungu viwili kwa udongo uleule; kimoja kwa matumizi ya heshima, na kingine kwa matumizi ya kawaida. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu. Alitaka kuonesha ghadhabu yake na kujulisha uwezo wake. Basi, alikuwa na saburi sana, akiwavumilia wale ambao walikuwa lengo la ghadhabu yake, ambao walistahili kuangamizwa. Alitaka pia kudhihirisha wingi wa utukufu wake ambao alitumiminia sisi tulio lengo la huruma yake; sisi ambao alikwisha kututayarisha kuupokea utukufu wake. Maana sisi ndio hao aliowaita, si kutoka miongoni mwa Wayahudi tu bali pia kutoka kwa watu wa mataifa mengine. Maana ndivyo asemavyo katika kitabu cha Hosea: “Wale waliokuwa ‘Si watu wangu’ nitawaita: ‘Watu wangu!’ Naye ‘Sikupendi’ ataitwa: ‘Mpenzi wangu!’ Na pale walipoambiwa: ‘Nyinyi si wangu’ hapo wataitwa: ‘Watoto wa Mungu aliye hai.’” Naye nabii Isaya, kuhusu Israeli anapaza sauti: “Hata kama wazawa wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaookolewa; maana, Bwana ataitekeleza upesi hukumu yake kamili juu ya ulimwengu wote.” Ni kama Isaya alivyosema hapo awali: “Bwana wa majeshi asingalituachia baadhi ya watoto wa Israeli, tungalikwisha kuwa kama Sodoma, tungalikwisha kuwa kama Gomora.” Basi tuseme nini? Watu wa mataifa ambao hawakutafuta wafanywe waadilifu, wamejaliwa kuwa waadilifu, kwa njia ya imani, hali watu wa Israeli ambao walitafuta sheria ya kuwafanya kuwa waadilifu, hawakuipata. Kwa nini? Kwa sababu walitegemea matendo yao badala ya kutegemea imani. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Tazama, nitaweka huko Siyoni jiwe likwazalo, mwamba utakaowafanya watu waanguke. Lakini atakayemwamini hataaibishwa!” Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima. Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli. Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe na hivyo hawakuikubali njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu. Maana kwa kuja kwake Kristo, sheria imefikia kikomo chake, ili wote wanaoamini wafanywe waadilifu. Kuhusu kuwa mwadilifu kwa kuitii sheria, Mose aliandika hivi: “Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya sheria ataishi.” Lakini kuhusu kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: “Usiseme moyoni mwako: ‘Nani atapanda mpaka mbinguni?’ (yaani, kumleta Kristo chini); wala usiseme: ‘Nani atashuka mpaka kuzimu?’ (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu).” Maandiko Matakatifu yasema hivi: “Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako” nao ndio ile imani tunayoihubiri. Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Maana mtu huamini kwa moyo akafanywa mwadilifu; na hukiri kwa kinywa akaokolewa. Maandiko Matakatifu yasema: “Kila anayemwamini hataaibishwa.” Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.” Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!” Lakini wote hawakuipokea hiyo habari njema. Maana Isaya alisema: “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” Hivyo basi, imani inatokana na kuusikia ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo. Lakini nauliza: Je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu.” Tena nauliza: Je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni wa kwanza kujibu: “Nitawafanyeni muwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu.” Tena Isaya anathubutu hata kusema: “Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionesha kwao wasiouliza habari zangu.” Lakini kuhusu Israeli anasema: “Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii.” Basi, nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? Hata kidogo! Mimi binafsi ni Mwisraeli, mzawa wa Abrahamu, wa kabila la Benyamini. Mungu hakuwakataa watu wake aliowateua tangu mwanzo. Mnakumbuka yasemavyo Maandiko Matakatifu juu ya Elia wakati alipomnungunikia Mungu kuhusu Israeli: “Bwana, wamewaua manabii wako na kubomoa madhabahu yako. Ni mimi tu peke yangu niliyebaki, nao wanataka kuniua!” Je, Mungu alimjibu nini? Alimwambia: “Nimejiwekea watu 7,000 ambao hawakumwabudu Baali.” Basi, ndivyo ilivyo pia wakati huu wa sasa: Ipo idadi ya waliobaki ambao Mungu aliwateua kwa sababu ya neema yake. Uteuzi wake unatokana na neema yake, na si kwa sababu ya matendo yao. Maana, kama uteuzi wake ungetegemea matendo ya watu, neema yake haingekuwa neema tena. Sasa, je? Watu wa Israeli hawakukipata kile walichokuwa wanakitafuta; lakini wote walioteuliwa walikipata. Wengine walipumbazwa, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mungu ameifanya mioyo yao kuwa mizito, na mpaka leo hii hawawezi kuona kwa macho yao wala kusikia kwa masikio yao.” Naye Daudi anasema: “Karamu zao na ziwe mtego wa kuwanasa, waanguke na kuadhibiwa. Macho yao yatiwe giza wasiweze kuona. Migongo yao ipindike kwa taabu daima!” Basi, nauliza: Je, Wayahudi wamejikwaa hata wakaangamia kabisa? Hata kidogo! Kutokana na kosa lao ukombozi umewajia watu wa mataifa mengine, ili Wayahudi wapate kuwaonea wivu. Kosa la Wayahudi limesababisha baraka nyingi kwa ulimwengu, na utovu wao wa kiroho umeleta baraka nyingi kwa watu wa mataifa mengine. Basi, ni dhahiri kwamba kuingizwa kwa idadi yao kamili kutakuwa ni baraka zaidi. Basi, sasa nawaambieni nyinyi watu wa mataifa mengine: Maadamu mimi nimekuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine, ninajivunia huduma yangu, nipate kuwafanya wananchi wenzangu wawaonee nyinyi wivu, na hivyo nipate kuwaokoa baadhi yao. Maana ikiwa kukataliwa kwao kulisababisha ulimwengu upatanishwe na Mungu, itakuwaje wakati watakapokubaliwa na Mungu? Wafu watafufuka! Ikiwa kipande cha kwanza cha mkate kimewekwa wakfu, mkate wote umewekwa wakfu; mizizi ya mti ikiwa mizuri, na matawi yake huwa mazuri pia. Naam, baadhi ya matawi ya mzeituni bustanini yalikatwa, na mahali pake tawi la mzeituni mwitu likapandikizwa. Nyinyi watu wa mataifa mengine ndio hilo tawi la mzeituni mwitu; na sasa mnashiriki nguvu na utomvu wa mzeituni bustanini. Basi, msiwadharau wale waliokatwa kama matawi! Na, hata kama kuna la kujivunia, kumbukeni kwamba si nyinyi mnaoitegemeza mizizi, bali mizizi ndiyo inayowategemeza nyinyi. Lakini utasema: “Matawi yalikatwa kusudi mimi nipandikizwe mahali pake.” Sawa! Yalikatwa kwa sababu ya kukosa imani, bali wewe unasimama kwa imani yako. Lakini usijivune; ila uwe na tahadhari. Kwa maana, ikiwa Mungu hakuwahurumia Wayahudi ambao ni kama matawi ya asili, je, unadhani atakuhurumia wewe? Ona, basi, jinsi Mungu alivyo mwema na mkali. Yeye ni mkali kwa wale walioanguka, na ni mwema kwako wewe ikiwa utaendelea katika wema wake; la sivyo, nawe pia utakatwa. Nao Wayahudi, hali kadhalika; wakiacha utovu wao wa imani, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena. Nyinyi watu wa mataifa mengine, kwa asili ni kama tawi la mzeituni mwitu, lakini mmeondolewa huko, mkapandikizwa katika mzeituni bustanini mahali ambapo kwa asili si penu. Lakini, Wayahudi kwa asili ni kama mzeituni bustanini, na itakuwa jambo rahisi zaidi kwao kupandikizwa tena katika mti huohuo wao. Ndugu zangu, napenda mjue ukweli huu uliofichika msije mkajiona wenye akili sana. Ukaidi wa Wayahudi ulikuwa ni wa muda tu, mpaka watu wa mataifa mengine watakapokuwa wamemfikia Mungu. Hapo ndipo taifa lote la Israeli litakapookolewa, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mkombozi atakuja kutoka Siyoni, atauondoa uovu wa wazawa wa Yakobo. Hili ndilo agano nitakalofanya nao wakati nitakapoziondoa dhambi zao.” Kwa sababu wanaikataa Habari Njema, Wayahudi wamekuwa maadui wa Mungu, lakini kwa faida yenu nyinyi watu wa mataifa. Lakini, kwa kuwa waliteuliwa, bado ni marafiki wa Mungu kwa sababu ya babu zao. Maana Mungu akisha wapa watu zawadi zake na kuwateua, hajuti kwamba amefanya hivyo. Hapo awali nyinyi mlikuwa mmemwasi Mungu, lakini sasa mmepata huruma yake kutokana na kuasi kwao. Hali kadhalika, kutokana na huruma mliyojaliwa nyinyi, Wayahudi wanamwasi Mungu sasa ili nao pia wapokee sasa huruma ya Mungu. Maana Mungu amewafunga watu wote katika uasi wao ili apate kuwahurumia wote. Utajiri, hekima na elimu ya Mungu ni kuu mno! Huruma zake hazichunguziki, na njia zake hazieleweki! Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Nani aliyepata kuyajua mawazo ya Bwana? Nani awezaye kuwa mshauri wake? Au, nani aliyempa yeye kitu kwanza hata aweze kulipwa tena kitu hicho?” Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, vyote vipo kwa uwezo wake na kwa ajili yake. Utukufu na uwe kwake hata milele! Amina. Kwa hiyo, ndugu zangu, maadamu Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: Mtoleeni Mungu miili yenu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu. Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu na kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu. Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni nyinyi nyote: Msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kadiri ya kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja. Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake. Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake. Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. Mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe. Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha. Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema. Pendaneni kindugu; kila mmoja amfikirie kwanza mwenzake kwa heshima. Msilegee katika bidii, ila muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana. Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima. Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu. Watakieni baraka wote wanaowadhulumu nyinyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani. Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wenye kulia. Ishini kwa kupatana vema nyinyi kwa nyinyi. Msijitakie makuu, bali jishughulisheni na madogo. Msijione kuwa wenye hekima sana. Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote. Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote. Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza, asema Bwana.” Zaidi ya hayo, Maandiko yasema: “Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake.” Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema. Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali; maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu. Anayepinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu; nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe. Maana, watawala hawasababishi hofu kwa watu wema, ila kwa watu wabaya. Basi, wataka usimwogope mtu mwenye mamlaka? Fanya mema naye atakusifu; maana yeye ni mtumishi wa Mungu anayefanya kazi kwa faida yako. Lakini ukifanya mabaya, basi, huna budi kumwogopa, maana anao kweli uwezo wa kuadhibu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, kuwaonesha ghadhabu yake wale watendao maovu. Kwa hiyo ni lazima kuwatii wenye mamlaka, si tu kwa sababu ya kuogopa ghadhabu ya Mungu, bali pia kwa sababu dhamiri inadai hivyo. Kwa sababu hiyohiyo nyinyi hulipa kodi; maana viongozi hao humtumikia Mungu ikiwa wanatimiza wajibu wao. Mpeni kila mtu haki yake; mtu wa ushuru, ushuru; wa kodi, kodi; na astahiliye heshima, heshima. Msiwe na deni kwa mtu yeyote, isipokuwa tu deni la kupendana. Ampendaye jirani yake ameitekeleza sheria. Maana, amri hizi: “Usizini; Usiue; Usitamani;” na nyingine zote, zimo katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Ampendaye jirani yake hamtendei vibaya. Basi, upendo ni utimilifu wa sheria. Zaidi ya hayo, nyinyi mnajua tumo katika wakati gani: Sasa ndio wakati wa kuamka usingizini; naam, wokovu wetu uko karibu zaidi sasa kuliko wakati ule tulipoanza kuamini. Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga. Na tuishi kwa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana, na wala sio kwa ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugomvi na wivu. Bwana Yesu Kristo awe vazi lenu; msishughulikie tena tamaa zenu za maumbile na kuziridhisha. Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane naye juu ya mawazo yake binafsi. Watu hutofautiana: Mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu; lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani. Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi kula kila kitu; naye ambaye hula tu mboga za majani asimhukumu anayekula kila kitu, maana Mungu amemkubali. Wewe ni nani hata uthubutu kumhukumu mtumishi wa mwingine? Akisimama au akianguka ni shauri la Bwana wake; naam, atasimama imara, maana Bwana anaweza kumsimamisha. Mtu anaweza kufikiria siku fulani kuwa ya maana zaidi kuliko nyingine; mtu mwingine aweza kuzifikiria siku zote kuwa sawa. Kila mmoja na afuate msimamo wa akili yake. Anayeadhimisha siku fulani anaadhimisha siku hiyo kwa ajili ya kumtukuza Mungu; naye anayekula chakula fulani anafanya hivyo kwa kumtukuza Bwana maana anamshukuru Mungu. Kadhalika naye anayeacha kula chakula fulani anafanya hivyo kwa ajili ya kumtukuza Bwana, naye pia anamshukuru Mungu. Maana hakuna mtu yeyote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana. Maana Kristo alikufa, akafufuka ili apate kuwa Bwana wa walio hai na wafu. Kwa nini basi, wewe wamhukumu ndugu yako? Nawe, kwa nini wamdharau ndugu yako? Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Maana Maandiko yanasema: “Kama niishivyo, asema Bwana, kila mtu atanipigia magoti, na kila mmoja atakiri kwamba mimi ni Mungu.” Kwa hiyo, kila mmoja wetu atatoa hoja juu yake mwenyewe mbele ya Mungu. Basi, tuache kuhukumiana, bali tuazimie kutokuwa kamwe kikwazo kwa ndugu au kumsababisha aanguke katika dhambi. Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake; lakini, mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi. Kama ukimhuzunisha ndugu yako kwa sababu ya chakula unachokula, basi mwenendo wako hauongozwi na upendo. Usikubali hata kidogo chakula chako kiwe sababu ya kupotea kwa mtu mwingine ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake! Basi, msikubali kitu mnachokiona kwenu kuwa chema kidharauliwe. Maana ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu. Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu, na kukubaliwa na watu. Kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani, na yanayotusaidia kujengana. Basi, usiiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya ubishi juu ya chakula. Vyakula vyote ni halali, lakini haifai kula chakula ambacho kitamfanya mtu aanguke katika dhambi. Afadhali kuacha kula nyama, kunywa divai, au kufanya chochote ambacho chaweza kumsababisha ndugu yako aanguke. Basi, shikilia unachoamini kati yako na Mungu wako. Heri mtu yule ambaye, katika kujiamulia la kufanya, haipingi dhamiri yake. Lakini mtu anayeona shaka juu ya chakula anachokula, anahukumiwa kama akila, kwa sababu msimamo wa kitendo chake haumo katika imani. Na, chochote kisicho na msingi wake katika imani ni dhambi. Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu. Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani. Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.” Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini. Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu, ili nyinyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni. Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia; ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Kwa hiyo nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa. Nitaziimba sifa za jina lako.” Tena Maandiko yasema: “Furahini, enyi watu wa mataifa; furahini pamoja na watu wake.” Na tena: “Enyi mataifa yote, msifuni Bwana; enyi watu wote, msifuni.” Tena Isaya asema: “Atatokea chipukizi katika ukoo wa Yese, naye atawatawala watu wa mataifa; nao watamtumainia.” Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba nyinyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana nyinyi kwa nyinyi. Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa tambiko inayokubaliwa na Mungu, tambiko iliyotakaswa na Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu. Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo, kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo. Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Watu wote ambao hawakuambiwa habari zake wataona; nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa.” Kwa sababu hiyo nilizuiwa mara nyingi kuja kwenu. Lakini maadamu sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu, natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi. Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalemu. Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoa mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalemu. Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia. Nitakapokwisha tekeleza kazi hiyo na kuwakabidhi mchango huo uliokusanywa kwa ajili yao, nitawatembeleeni nyinyi nikiwa safarini kwenda Spania. Najua ya kuwa nikija kwenu nitawaletea wingi wa baraka za Kristo. Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo uletwao na Roho, mniunge mkono kwa kuniombea kwa Mungu. Ombeni nipate kutoka salama miongoni mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, nayo huduma yangu huko Yerusalemu ipate kukubaliwa na watu wa Mungu walioko huko. Hivyo, Mungu akipenda, nitaweza kuja kwenu na moyo wa furaha, nikapumzike pamoja nanyi. Mungu aliye chanzo cha amani na awe nanyi nyote! Amina! Napenda kumjulisha kwenu dada yetu Foibe ambaye ni mtumishi katika kanisa la Kenkrea. Mpokeeni kwa ajili ya Bwana kama iwapasavyo watu wa Mungu. Mpeni msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, maana yeye amekuwa mwema sana kwa watu wengi na kwangu pia. Salamu zangu ziwafikie Priska na Akula, wafanyakazi wenzangu katika utumishi wa Kristo Yesu. Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu. Wanastahili shukrani; si tu kutoka kwangu, bali pia kutoka kwa makanisa yote ya watu wa mataifa mengine. Salamu zangu pia kwa kanisa linalokutana nyumbani kwao. Salamu zangu zimfikie rafiki yangu Epaineto ambaye ni wa kwanza katika mkoa wa Asia kumwamini Kristo. Nisalimieni Maria ambaye amefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu. Salamu zangu kwa Androniko na Yunia, wananchi wenzangu waliofungwa gerezani pamoja nami; wao wanajulikana sana kati ya mitume; tena walikuwa Wakristo kabla yangu mimi. Salamu zangu kwa Ampliato, rafiki yangu katika kuungana na Bwana. Salamu zangu zimfikie Urbano, mfanyakazi mwenzangu katika utumishi wa Kristo; salamu zangu pia kwa rafiki yangu Staku. Nisalimieni Apele ambaye uaminifu wake kwa Kristo umethibitishwa. Salamu zangu kwa wote walio nyumbani mwa Aristobulo. Salamu zangu kwa Herodiana, mwananchi mwenzangu; na kwa jamaa yote ya Narkisi iliyojiunga na Bwana. Nisalimieni Trufena na Trufosa wanaofanya kazi katika utumishi wa Bwana, na rafiki yangu Persi ambaye amefanya mengi kwa ajili ya Bwana. Nisalimieni Rufo, mtu hodari sana katika kazi ya Bwana, na mama yake ambaye ni mama yangu pia. Nisalimieni Asunkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao. Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa, pamoja na watu wote wa Mungu walio pamoja nao. Salimianeni nyinyi kwa nyinyi kwa ishara ya upendo. Salamu kwenu kutoka kwa makanisa yote ya Kristo. Ndugu zangu, nawasihi mwafichue wote wanaosababisha mafarakano na kuwafanya watu wengine waanguke, kinyume cha mafundisho mliyofundishwa. Jiepusheni na watu hao, maana watu wa namna hiyo hawamtumikii Kristo Bwana wetu, bali wanayatumikia matumbo yao wenyewe. Kwa maneno yao matamu na hotuba za kubembeleza hupotosha mioyo ya watu wanyofu. Kila mtu amesikia juu ya utii wenu katika mambo mema, na bila hatia kuhusu mambo mabaya. Naye Mungu aliye chanzo cha amani hatakawia kumponda Shetani chini ya miguu yenu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Timotheo, mfanyakazi mwenzangu, anawasalimu. Hali kadhalika Lukio, Yasoni, na Sosipateri, wananchi wenzangu, wanawasalimu. Nami Tertio, ninayeandika barua hii, nawasalimuni kwa jina la Bwana. Gayo, mwenyeji wangu, pamoja na kanisa lote linalokutana kwake, anawasalimu. Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto, wanawasalimu. [ Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amina.] Basi, sasa na tumsifu Mungu! Yeye anaweza kuwaimarisheni katika ile Habari Njema niliyohubiri juu ya Yesu Kristo, na katika ile siri iliyofunuliwa na ambayo ilikuwa imefichika kwa karne nyinyi zilizopita. Lakini, sasa ukweli huo umefunuliwa kwa njia ya maandiko ya manabii; na kwa amri ya Mungu wa milele umedhihirishwa kwa mataifa yote ili wote waweze kuamini na kutii. Kwake Mungu aliye peke yake mwenye hekima, uwe utukufu kwa njia ya Yesu Kristo, milele na milele! Amina. Mimi Paulo, niliyeitwa kuwa mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Sosthene, tunawaandikia nyinyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho. Nyinyi mmefanywa watakatifu katika kuungana na Kristo Yesu, mkaitwa muwe watu wa Mungu, pamoja na watu wote popote wanaomwomba Bwana wetu Yesu Kristo aliye Bwana wao na wetu pia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo. Ninamshukuru Mungu wangu daima kwa ajili yenu kwa sababu amewatunukia nyinyi neema yake kwa njia ya Kristo Yesu. Maana, kwa kuungana na Kristo mmetajirishwa katika kila kitu. Mmejaliwa elimu yote na uwezo wote wa kuhubiri. Maana ujumbe juu ya Kristo umethibitishwa ndani yenu, hata hampungukiwi kipaji chochote cha kiroho mkiwa mnangojea kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye atawaimarisheni nyinyi mpaka mwisho mpate kuonekana bila hatia siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita nyinyi muwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu. Ndugu, nawasihini kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo: Pataneni nyote katika kila jambo msemalo; yasiweko mafarakano kati yenu; muwe na fikira moja na nia moja. Ndugu zangu, habari nilizopata kutoka kwa watu kadhaa wa jamaa ya Kloe, zaonesha wazi kwamba kuna kutoelewana kati yenu. Nataka kusema hivi: Kila mmoja anasema chake: Mmoja husema, “Mimi ni wa Paulo”, mwingine: “Mimi ni wa Apolo”, mwingine: “Mimi ni wa Kefa,” na mwingine: “Mimi ni wa Kristo.” Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? Namshukuru Mungu kwamba sikumbatiza mtu yeyote miongoni mwenu isipokuwa tu Krispo na Gayo. Kwa hiyo hakuna awezaye kusema amebatizwa kwa jina langu. ( Samahani, nilibatiza pia jamaa ya Stefana; lakini zaidi ya hawa, sidhani kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote). Kristo hakunituma kubatiza, bali kuhubiri Habari Njema; tena, niihubiri bila kutegemea maarifa ya hotuba za watu, kusudi nguvu ya kifo cha Kristo msalabani isibatilishwe. Maana ujumbe kuhusu kifo cha Kristo msalabani ni jambo la kipumbavu kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea, lakini kwetu sisi tulio katika njia ya wokovu, ujumbe huo ni nguvu ya Mungu. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, na elimu ya wataalamu nitaitupilia mbali.” Yu wapi basi, mwenye hekima? Yu wapi basi, mwalimu wa sheria? Naye bingwa wa mabishano wa nyakati hizi yuko wapi? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upumbavu. Maana, kadiri ya hekima ya Mungu, watu hawawezi kumjua Mungu kwa njia ya hekima yao wenyewe. Badala yake, Mungu amependa kuwaokoa wale wanaoamini kwa njia ya kile ambacho wenye hekima wanakiona kuwa ni upumbavu, yaani ujumbe tunaohubiri. Wayahudi wanataka ishara, na Wagiriki wanatafuta hekima; lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa. Kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo, na kwa watu wa mataifa ni upumbavu; lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu kuliko nguvu za binadamu. Ndugu, kumbukeni wakati mlipoitwa: Wengi wenu hawakuwa wenye hekima hata kwa fikira za binadamu; wengi hawakuwa wenye nguvu au watu wa tabaka la juu. Ndiyo kusema, Mungu aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni upumbavu, ili awaaibishe wenye hekima; na aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni dhaifu, ili awaaibishe wenye nguvu. Mungu ameyachagua yale ambayo kwa fikira za dunia ni mambo yaliyo duni na yanayodharauliwa, mambo ambayo hata hayakuwako, ili kwa hayo ayafutilie mbali yale ambayo kwa fikira za binadamu ni mambo ya maana. Basi, hakuna mtu awezaye kujivunia chochote mbele ya Mungu. Mungu mwenyewe ndiye aliyewaunganisha nyinyi na Kristo Yesu. Mungu amemfanya Kristo awe hekima yetu; kwa njia yake sisi tunapatanishwa na Mungu, tunakuwa watu wake Mungu na kukombolewa. Basi, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mwenye kutaka kujivuna, na ajivunie kazi ya Bwana.” Ndugu, mimi nilipokuja kwenu sikuwahubiria siri ya ujumbe wa Mungu kwa ufasaha wa lugha, au kwa hekima ya binadamu. Nilipokuwa kwenu niliamua kutojua chochote kile isipokuwa tu kumjua Yesu Kristo; naam, Kristo aliyesulubiwa. Nilipokuwa kwenu nilikuwa dhaifu, natetemeka kwa hofu nyingi. Hotuba zangu na mahubiri yangu sikuyatoa kwa maneno ya kuvutia na ya hekima, bali kwa uthibitisho mwingi na nguvu ya Roho. Nilifanya hivyo kusudi imani yenu ipate kutegemea nguvu ya Mungu, na si hekima ya binadamu. Hata hivyo, sisi tunatumia lugha ya hekima kwa wale waliokomaa kiroho; lakini hekima hiyo si ya hapa duniani, wala si ya watawala wa dunia hii ambao wako katika mkumbo wa kupotea. Hekima tunayotumia ni hekima ya siri ya Mungu, hekima iliyofichika, ambayo Mungu aliiazimia tangu mwanzo kwa ajili ya utukufu wetu. Ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana wangaliielewa, hawangalimsulubisha Bwana wa utukufu. Lakini, ni kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona, wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao.” Hayo ndiyo mambo Mungu aliyotufunulia kwa njia ya Roho wake. Maana Roho huchunguza kila kitu hata mambo ya ndani kabisa ya Mungu. Nani awezaye kujua mambo ya ndani ya mtu isipokuwa roho yake mtu huyo? Hali kadhalika, hakuna ajuaye mambo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. Sasa, sisi hatukuipokea roho ya ulimwengu, bali tumepokea Roho atokaye kwa Mungu ili atuwezeshe kujua yale tuliyojaliwa na Mungu. Basi, sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa na hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho. Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtupu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho. Lakini mtu aliye na huyo Roho anaweza kubainisha ubora wa kila kitu, naye mwenyewe hahukumiwi na mtu mwingine. Maandiko yasema: “Nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Nani awezaye kumshauri?” Lakini sisi tunayo akili ya Kristo. Ndugu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu mlio na huyo Roho. Nilipaswa kusema nanyi kama watu wa kidunia, kama watoto wachanga katika maisha ya Kikristo. Ilinibidi kuwalisheni kwa maziwa, na si kwa chakula kigumu, kwani hamkuwa tayari kukipokea. Hata sasa hamko tayari. Maana bado nyinyi ni watu wa kidunia. Je, si kweli kwamba bado uko wivu na ugomvi kati yenu? Mambo hayo yanaonesha wazi kwamba nyinyi bado ni watu wa kidunia, mnaishi mtindo wa kidunia. Mmoja wenu anaposema, “Mimi ni wa Paulo”, na mwingine, “Mimi ni wa Apolo”, je, hiyo haionyeshi kwamba mnaishi bado kama watu wa dunia hii tu? Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Sisi ni watumishi tu ambao tuliwaleteeni nyinyi imani. Kila mmoja wetu anafanya kazi aliyopewa na Bwana. Mimi nilipanda mbegu, Apolo akamwagilia maji; lakini aliyeiotesha mbegu ni Mungu. Wa maana si yule aliyepanda mbegu, au yule aliyemwagilia maji; wa maana ni Mungu aliyeiwezesha mbegu kuota. Yule aliyepanda na yule aliyemwagilia maji wote ni sawa, ingawa kila mmoja atapokea tuzo lake kufuatana na jitihada yake mwenyewe. Maana sisi ni ndugu, wafanyakazi pamoja na Mungu; na nyinyi ni shamba lake; nyinyi ni jengo lake. Kwa msaada wa neema aliyonipa Mungu, nimefaulu, kama mwashi stadi mwenye busara, kuweka msingi ambao juu yake mtu mwingine anajenga. Basi, kila mmoja awe mwangalifu jinsi anavyojenga juu yake. Hakuna mtu awezaye kuweka msingi mwingine badala ya ule uliokwisha wekwa, yaani Yesu Kristo. Juu ya msingi huo mtu anaweza kujenga kwa dhahabu, fedha au mawe ya thamani; anaweza kutumia miti, majani au nyasi. Iwe iwavyo, ubora wa kazi ya kila mmoja utaonekana wakati siku ile ya Kristo itakapoifichua. Maana, siku hiyo itatokea na moto, na huo moto utaipima na kuonesha ubora wake. Ikiwa alichojenga mtu juu ya huo msingi kitaustahimili huo moto, atapokea tuzo; lakini kama alichojenga kitaunguzwa, basi, atapoteza tuzo lake; lakini yeye mwenyewe ataokolewa kana kwamba ameponyoka kutoka motoni. Je, hamjui kwamba nyinyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Basi, mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu; maana hekalu la Mungu ni takatifu, na hekalu hilo ni nyinyi wenyewe. Msijidanganye! Mtu yeyote miongoni mwenu akijidhania mwenye hekima mtindo wa kidunia, heri awe mjinga kusudi apate kuwa na hekima ya kweli. Maana, hekima ya kidunia ni upumbavu mbele ya Mungu. Kwani Maandiko Matakatifu yasema: “Mungu huwanasa wenye hekima katika ujanja wao.” Na tena: “Bwana ajua kwamba mawazo ya wenye hekima hayafai.” Basi, mtu asijivunie watu. Maana kila kitu ni chenu. Paulo, Apolo na Kefa, ulimwengu, maisha na kifo; mambo ya sasa na ya baadaye, yote ni yenu. Lakini nyinyi ni wa Kristo, naye Kristo ni wa Mungu. Mtu na atuone sisi kuwa ni watumishi wa Kristo tuliokabidhiwa siri za Mungu. Kinachotakiwa kwa yeyote yule aliyekabidhiwa kazi ni kuwa mwaminifu. Kwangu mimi si kitu nikihukumiwa na nyinyi, au na mahakama ya kibinadamu; wala sijihukumu mimi mwenyewe. Dhamiri yangu hainishtaki kwa jambo lolote, lakini hiyo haionyeshi kwamba sina lawama. Bwana ndiye anayenihukumu. Basi, msihukumu kabla ya wakati wake; acheni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayafichua mambo ya giza yaliyofichika, na kuonesha wazi nia za mioyo ya watu. Ndipo kila mmoja atapata sifa anayostahili kutoka kwa Mungu. Ndugu, hayo yote niliyosema juu ya Apolo na juu yangu, ni kielelezo kwenu: Kutokana na mfano wangu mimi na Apolo nataka mwelewe maana ya msemo huu: “Zingatieni yaliyoandikwa.” Kati yenu pasiwe na mtu yeyote anayejivunia mtu mmoja na kumdharau mwingine. Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukukipewa? Haya! Mmekwisha shiba! Mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme bila ya sisi! Naam, laiti mngekuwa kweli watawala, ili nasi pia tutawale pamoja nanyi. Nafikiri Mungu ametufanya sisi mitume tuwe watu wa mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kuuawa, maana tumekuwa tamasha mbele ya ulimwengu wote, mbele ya malaika na watu. Sisi ni wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini nyinyi ni wenye busara katika kuungana na Kristo! Sisi ni dhaifu, nyinyi ni wenye nguvu. Nyinyi mnaheshimika, sisi tunadharauliwa. Mpaka dakika hii, sisi tuna njaa na kiu, hatuna nguo, twapigwa makofi, hatuna malazi. Tena twataabika na kufanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa, tunawatakia baraka; tukidhulumiwa, tunavumilia; tukisingiziwa, tunajibu kwa adabu. Mpaka sasa tumetendewa kama uchafu wa dunia; na kwa kila mtu sisi ni takataka! Siandiki mambo haya kwa ajili ya kuwaaibisha nyinyi, bali kwa ajili ya kuwafundisheni watoto wangu wapenzi. Maana hata kama mnao maelfu ya walezi katika maisha yenu ya Kikristo, baba yenu ni mmoja tu, kwani katika kuungana na Kristo mimi ndiye niliyewazaeni kwa kuihubiri Habari Njema. Kwa hiyo, nawasihi: Fuateni mfano wangu. Ndiyo maana nimemtuma Timotheo kwenu. Yeye ni mtoto wangu mpenzi na mwaminifu katika kuungana na Bwana. Atawakumbusheni njia ninayofuata katika kuungana na Kristo; njia ninayofundisha kila mahali katika makanisa yote. Baadhi yenu wameanza kuwa na majivuno wakidhani kwamba sitakuja tena kwenu. Lakini, Bwana akipenda, nitakuja kwenu upesi; na hapo ndipo nitakapojionea mwenyewe, sio tu kile wanachoweza kusema hao wenye majivuno, bali pia kile wanachoweza kufanya. Maana ufalme wa Mungu si shauri la maneno matupu, bali ni nguvu. Mnapendelea lipi? Nije kwenu na fimbo, ama nije na moyo wa upendo na upole? Ziko habari za kuaminika kwamba kuna uzinzi miongoni mwenu; tena ni uzinzi mbaya ambao haujapata kuwako hata kati ya watu wasiomjua Mungu. Nimeambiwa eti mmoja wenu anaishi na mke wa baba yake! Mnawezaje kujivuna? Ingekuwa afadhali kwenu kuomboleza, na huyo aliyefanya kitu hicho aondolewe miongoni mwenu. Nami, kwa upande wangu, ingawa kwa mwili niko mbali nanyi, hata hivyo kwa roho niko hapo pamoja nanyi: Na hivyo, kama vile nipo hapo, nimekwisha mhukumu huyo aliyefanya jambo hilo la aibu. Wakati mnapokusanyika pamoja kwa jina la Bwana Yesu, nami nikiwa pamoja nanyi kwa roho, basi, kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu, mkabidhini mtu huyo kwa Shetani ili mwili wake uharibiwe na roho yake iweze kuokolewa siku ile ya Bwana. Majivuno yenu hayafai! Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge lote la unga? Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa kuwa sadaka. Basi, tufanye karamu hiyo si kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, mkate wa usafi na kweli. Niliwaandikia katika barua yangu msishirikiane na wazinzi. Ukweli ni kwamba sikuwa na maana ya watu wote duniani walio wazinzi, wachoyo, walaghai na wenye kuabudu sanamu. Maana, ili kuwaepa hao wote ingewalazimu nyinyi kuihama dunia hii kabisa! Nilichoandika ni hiki: Msishirikiane na ndugu Mkristo aliye mzinzi, mchoyo, mwenye kuabudu sanamu, mchongezi, mlevi na mlaghai. Mtu wa namna hiyo, hata kula msile naye. Je, ni shauri langu kuwahukumu watu walio nje? Hao Mungu atawahukumu. Je, nyinyi hampaswi kuwahukumu wale walio katika jamii yenu nyinyi wenyewe? Mfukuzeni mbali nanyi huyo mwovu! Anathubutuje mmoja wenu kumshtaki ndugu mwaamini mbele ya mahakama ya watu wasiomjua Mungu badala ya kumshtaki mbele ya watu wa Mungu? Je, hamjui kwamba watu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Ikiwa basi, ulimwengu utahukumiwa nanyi, kwa nini hamstahili kuhukumu hata katika mambo madogo? Je, hamjui kwamba, licha ya kuhukumu mambo ya kawaida ya kila siku, tutawahukumu hata malaika? Mnapokuwa na mizozo juu ya mambo ya kawaida, je, mnawaita wawe mahakimu watu ambao hata hawalijali kanisa? Aibu kwenu! Ndiyo kusema hakuna hata mmoja miongoni mwenu mwenye hekima kiasi cha kuweza kutatua tatizo kati ya ndugu waumini? Badala yake, kweli imekuwa mtindo ndugu kumpeleka ndugu yake mahakamani, tena mbele ya mahakimu wasioamini. Kwa kweli huko kushtakiana tu wenyewe kwa wenyewe kwabainisha kwamba mmeshindwa kabisa! Je, haingekuwa jambo bora zaidi kwenu kudhulumiwa? Haingekuwa bora zaidi kwenu kunyanganywa mali yenu? Lakini, badala yake, nyinyi ndio mnaodhulumu na kunyanganya; tena, hayo mnawafanyia ndugu zenu! Au je, hamjui kwamba watu wabaya hawataurithi ufalme wa Mungu? Msijidanganye! Watu wanaoishi maisha ya uasherati, wanaoabudu sanamu, wazinzi, au walawiti, wezi, wachoyo, walevi, wasengenyaji, wanyanganyi, hao wote hawatashiriki ufalme wa Mungu. Baadhi yenu mlikuwa hivyo; lakini sasa mmeoshwa, mkafanywa watakatifu, na kufanywa waadilifu na kupatanishwa na Mungu kwa jina la Bwana Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu. Mtu anaweza kusema: “Kwangu mimi kila kitu ni halali.” Sawa; lakini si kila kitu kinafaa. Nakubali kwamba kila kitu ni halali kwangu lakini sitaki kutawaliwa na kitu chochote. Unaweza kusema: “Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula.” Sawa; lakini Mungu ataviharibu vyote viwili. Mwili wa mtu si kwa ajili ya uzinzi bali ni kwa ajili ya kumtumikia Bwana, naye Bwana ni kwa ajili ya mwili. Basi, Mungu aliyemfufua Bwana kutoka wafu atatufufua nasi pia kwa nguvu yake. Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya mwili wa Kristo? Je, mnadhani naweza kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuifanya kuwa sehemu ya mwili wa kahaba? Hata kidogo! Maana, kama mjuavyo, anayeungana na kahaba huwa mwili mmoja naye — kama ilivyoandikwa: “Nao wawili watakuwa mwili mmoja.” Lakini aliyejiunga na Bwana huwa roho moja naye. Jiepusheni kabisa na uzinzi. Dhambi nyingine zote hutendwa nje ya mwili lakini mzinzi hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe. Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, ambaye mlimpokea kutoka kwa Mungu? Nyinyi basi, si mali yenu wenyewe. Mlinunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo, itumieni miili yenu kwa ajili ya kumtukuza Mungu. Yahusu sasa mambo yale mliyoandika: Naam, ni vizuri kama mtu haoi; lakini kwa sababu ya hatari ya uzinzi, basi, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. Mume atimize wajibu alio nao kwa mkewe, naye mke atimize wajibu alio nao kwa mumewe. Mke hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mumewe anayo; hali kadhalika naye mume, hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mkewe anayo. Msinyimane haki zenu, isipokuwa kama mnaafikiana kufanya hivyo kwa kitambo tu, ili mpate nafasi nzuri ya kusali. Kisha rudianeni tena mara, ili Shetani asije akawajaribuni kwa sababu ya udhaifu wenu. Ninayowaambieni sasa ni mawaidha, si amri. Ningependa watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mmoja anacho kipaji chake kutoka kwa Mungu; mmoja kipaji hiki na mwingine kile. Basi, wale ambao hawajaoa na wale walio wajane nawaambia kwamba ni vema kuendelea kuwa kama mimi nilivyo. Hata hivyo, kama mtu hawezi kujizuia, basi na aoe; maana ni afadhali zaidi kuoa kuliko kuwaka tamaa. Kwa wale waliooa ninayo amri, tena si yangu, ila ni ya Bwana: Mke asiachane na mumewe; lakini kama akiachana naye, basi abaki bila kuolewa; ama la, apatanishwe na mume wake. Mume naye asimpe talaka mkewe. Kwa wale wengine, (mimi binafsi, si Bwana) nasema hivi: Ikiwa mwanamume Mkristo anaye mke asiyeamini, na huyo mwanamke akakubali kuendelea kuishi naye, asimpe talaka. Na, kama mwanamke Mkristo anaye mume asiyeamini, na huyo mwanamume akakubali kuendelea kuishi naye, basi, asimpe talaka mumewe. Kwa maana huyo mume asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mkewe; na huyo mke asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mumewe. Vinginevyo watoto wao wangekuwa si wa Mungu; kumbe sasa ni watoto wake Mungu. Hata hivyo, ikiwa yule asiyeamini anataka kumwacha mwenzake aliye Mkristo, basi, na amwache tu. Hapo huyo Mkristo, mume au mke, atakuwa huru. Maana Mungu amewaiteni nyinyi muishi kwa amani. Wewe mama Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mume wako? Au wewe mume Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mkeo? Kwa vyovyote kila mmoja na aishi kufuatana na vipaji alivyogawiwa na Bwana, na kama alivyoitwa na Mungu. Hili ndilo agizo langu kwa makanisa yote. Kama mtu aliitwa akiwa ametahiriwa, basi asijisingizie kwamba hakutahiriwa; na kama alipoitwa hakuwa ametahiriwa, basi na asitahiriwe. Maana kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; kilicho muhimu ni kuzishika amri za Mungu. Basi, kila mmoja na abaki kama alivyokuwa wakati alipoitwa. Je, wewe ulikuwa mtumwa wakati ulipoitwa? Sawa, usijali; lakini ukipata fursa ya kuwa huru, itumie. Maana yeye aliyeitwa na Bwana akiwa mtumwa huyo huwa mtu huru wa Bwana. Hali kadhalika naye aliyeitwa akiwa mtu huru, huwa mtumwa wa Kristo. Nyote mmenunuliwa kwa bei; kwa hiyo msiwe tena watumwa wa watu. Ndugu zangu, kila mmoja wenu basi, na abaki na Mungu kama alivyokuwa wakati alipoitwa. Sasa, kuhusu mabikira na waseja, sina amri kutoka kwa Bwana; lakini natoa maoni yangu mimi ambaye kwa huruma yake Bwana nastahili kuaminiwa. Basi, kutokana na shida iliyopo sasa nadhani ingefaa mtu abaki kama alivyo. Je, umeoa? Basi, usitake kuachana na mkeo. Wewe hukuoa? Basi, usitake kuoa. Lakini ikiwa utaoa hutakuwa umetenda dhambi; na msichana akiolewa hatakuwa ametenda dhambi. Hao watakaooana watapatwa na matatizo ya dunia hii, lakini mimi ningependa hayo yasiwapate nyinyi. Ndugu, nataka kusema hivi: Muda uliobaki ni mfupi. Na tangu sasa wale waliooa na waishi kama vile hawakuoa; wenye kulia wawe kama hawalii, na wenye kufurahi wawe kama hawafurahi; wanaonunua wawe kama hawana kitu; nao wenye shughuli na dunia hii wawe kama vile hawana shughuli sana nayo. Maana ulimwengu huu, kama tuujuavyo, unapita. Ningependa nyinyi msiwe na wasiwasi. Mtu asiye na mke hujishughulisha na kazi ya Bwana jinsi atakavyompendeza Bwana. Mwanamume aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia jinsi atakavyompendeza mkewe, naye amegawanyika. Mwanamke asiyeolewa au bikira hujishughulisha na mambo ya Bwana apate kujitolea mwili na roho kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii jinsi atakavyompendeza mumewe. Nawaambieni haya kwa faida yenu, na si kwa kuwawekeeni kizuizi. Nataka tu muwe na mpango unaofaa, mpate kumtumikia Bwana kwa moyo na nia moja. Kama mtu anaona kwamba hamtendei vyema mchumba wake asipomwoa, na kama tamaa zake zinamshinda, na afanye atakavyo; waoane tu; hatakuwa ametenda dhambi. Lakini kama huyo mwanamume akiamua kwa hiari moyoni mwake kutooa na kama anaweza kuzitawala tamaa zake na kuamua namna ya kufanya, basi, anafanya vizuri zaidi asipomwoa huyo mwenzake bikira. Kwa maneno mengine: Yule anayeamua kuoa anafanya vema; naye anayeamua kutooa anafanya vema zaidi. Mwanamke aliyeolewa huwa amefungwa na mumewe kwa muda wote mumewe aishipo. Lakini mumewe akifa, mama huyo yuko huru, na akipenda anaweza kuolewa na mtu yeyote, mradi tu iwe Kikristo. Lakini, nionavyo mimi, atakuwa na heri zaidi kama akibaki hivyo alivyo. Hayo ni maoni yangu, na nafikiri mimi pia ninaye Roho wa Mungu. Yahusu sasa vyakula vilivyotambikiwa sanamu: Tunajua kwamba sisi sote tuna ujuzi, lakini ujuzi huo huwafanya watu wawe na majivuno; lakini mapendo hujenga. Anayefikiri kwamba anajua kitu, kwa kweli hajui chochote kama inavyompasa. Lakini anayempenda Mungu, huyo anajulikana naye. Kwa hiyo, kuhusu vyakula vilivyotambikiwa sanamu, twajua kwamba sanamu si kitu duniani; twajua kwamba Mungu ni mmoja tu. Hata kama viko vitu viitwavyo miungu duniani au mbinguni, na hata kama wako miungu na mabwana wengi, hata hivyo, kwetu sisi yuko Mungu mmoja tu; Baba, Muumba wa vyote, ambaye kwa ajili yake sisi tuko. Pia yuko Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa njia yake vitu vyote viliumbwa, na sisi twaishi kwa njia yake. Lakini, si kila mtu anao ujuzi huu. Maana wako watu wengine waliokwisha zoea sanamu, watu ambao mpaka hivi sasa wanapokula vyakula huviona bado kama vyakula vilivyotambikiwa sanamu. Na kwa vile dhamiri zao ni dhaifu, hutiwa unajisi. Lakini chakula hakiwezi kutupeleka karibu zaidi na Mungu. Tukiacha kukila hatupungukiwi kitu, tukikila hatuongezewi kitu. Lakini, jihadharini: Huu uhuru wenu usiwafanye walio na imani dhaifu waanguke katika dhambi. Maana, mtu ambaye dhamiri yake ni dhaifu, akikuona wewe mwenye ujuzi unakula vyakula hivyo ndani ya hekalu la sanamu, je, hatatiwa moyo wa kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu? Hivyo, huyo ndugu yako dhaifu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, atapotea kwa sababu ya ujuzi wako. Kama mkiwakosesha ndugu zenu jinsi hiyo, na kuzijeruhi dhamiri zao dhaifu, mtakuwa mmemkosea Kristo. Kwa hiyo, ikiwa chakula husababisha kuanguka kwa ndugu yangu, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi. Je, mimi si mtu huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Je, nyinyi si matokeo ya kazi yangu kwa ajili ya Bwana? Hata kama kwa watu wengine mimi si mtume, lakini walau kwenu nyinyi mimi ni mtume. Nyinyi ni uthibitisho wa utume wangu kwa sababu ya kuungana kwenu na Bwana. Hoja yangu kwa wale wanaonipinga ndiyo hii: Je, hatuna haki ya kula na kunywa? Je, hatuna ruhusa kumchukua mke Mkristo katika ziara zetu, kama vile wafanyavyo mitume wengine, ndugu zake Bwana, na pia Kefa? Au ni mimi tu na Barnaba ambao tunapaswa kujipatia maslahi yetu kwa kufanya kazi? Je, mwanajeshi gani anayelipia utumishi wake jeshini? Mkulima gani asiyekula matunda ya shamba lake la mizabibu? Mchungaji gani asiyekunywa maziwa ya mifugo yake? Je, nasema mambo haya kibinadamu tu? Je, sheria nayo haisemi hivyo? Imeandikwa katika sheria: “Usimfunge kinywa ng'ombe anapopura nafaka.” Je, ndio kusema Mungu anajishughulisha na ng'ombe? Je, hakuwa anatufikiria sisi aliposema hivyo? Naam, haya yaliandikwa kwa ajili yetu; maana yule anayelima na yule anayevuna, wote wawili wana haki ya kutumaini kupata sehemu ya mavuno. Ikiwa sisi tumepanda mbegu ya kiroho kati yenu, je, ni jambo kubwa tukichuma kwenu faida ya kidunia? Ikiwa wengine wanayo haki ya kutazamia hayo kutoka kwenu, je, sisi hatuna haki zaidi kuliko hao? Lakini, sisi hatukuitumia haki hiyo. Badala yake, tumestahimili kila kitu ili tusiiwekee kizuizi chochote Habari Njema ya Kristo. Je, hamjui kwamba wanaotumikia hekaluni hupata chakula chao hekaluni, na kwamba wanaotoa sadaka madhabahuni hupata sehemu ya hiyo sadaka? Bwana aliagiza vivyo hivyo; wahubiri wa Habari Njema wapate riziki zao kutokana nayo. Lakini, mimi sikutumia hata mojawapo ya haki hizo. Na wala siandiki nijipatie haki hizo; kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kumfanya yeyote aone kwamba najisifu bure. Ikiwa ninaihubiri injili, hilo si jambo la kujivunia; hilo ni jukumu nililopewa. Na, ole wangu kama sitaihubiri injili! Ningekuwa nimeichagua kazi hii kwa hiari, basi, ningetazamia malipo; lakini maadamu naifanya ikiwa ni wajibu, hiyo ina maana kwamba ni jukumu nililopewa nitekeleze. Mshahara wangu ni kitu gani, basi? Mshahara wangu ni fursa ya kuihubiri Habari Njema bure, bila kudai haki ninazostahili kwa kuihubiri. Kwa hiyo, ingawa mimi si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya mtumwa wa kila mtu ili nimpatie Kristo watu wengi iwezekanavyo. Kwa Wayahudi nimeishi kama Myahudi ili niwapate Wayahudi; yaani, ingawa mimi siko chini ya sheria, nimejiweka chini ya sheria kwao, ili niwapate hao walio chini ya sheria. Na kwa wale walio nje ya sheria, naishi kama wao, nje ya sheria, ili niwapate hao walio nje ya sheria. Hii haimaanishi kwamba mimi niko nje ya sheria ya Mungu, maana nabanwa na sheria ya Kristo. Kwao walio dhaifu nimejifanya dhaifu ili niwapate hao walio dhaifu. Nimejifanya kila kitu kwa wote ili nipate kuwaokoa baadhi yao kwa kila njia. Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, nipate kushiriki baraka zake. Je, hamjui kwamba katika uwanja wa michezo, ingawa wapiga mbio wote hukimbia, ni mmoja tu anayejinyakulia zawadi? Wanariadha hujipa mazoezi na nidhamu kali; hufanya hivyo ili wajipatie taji iharibikayo! Lakini sisi twafanya hivyo tupate taji isiyoharibika. Ndivyo basi, ninavyopiga mbio nikiwa na nia ya kushinda; ndivyo ninavyopigana, na si kama bondia anayetupa ngumi zake hewani. Naupa mwili wangu mazoezi magumu na kuutia katika nidhamu kamili, nisije mimi mwenyewe nikakataliwa baada ya kuwahubiria wengine. Ndugu, nataka mjue kwamba babu zetu wote walikuwa chini ya ulinzi wa lile wingu, na kwamba wote walivuka salama ile bahari. Wote walibatizwa katika umoja na Mose katika lile wingu na katika ile bahari. Wote walikula chakula kilekile cha kiroho, wakanywa pia kinywaji kilekile cha kiroho, maana walikunywa kutoka ule mwamba wa kiroho uliowafuata; mwamba huo ulikuwa Kristo mwenyewe. Hata hivyo, wengi wao hawakumpendeza Mungu, na maiti zao zilisambazwa jangwani. Sasa, mambo hayo yote ni mfano tu kwetu; yanatuonya sisi tusitamani ubaya kama wao walivyotamani. Msiwe waabudu sanamu kama baadhi yao walivyokuwa; kama yasemavyo Maandiko: “Watu waliketi kula na kunywa, wakasimama kucheza.” Wala tusizini kama baadhi yao walivyozini, wakaangamia siku moja watu 23,000. Tusimjaribu Bwana kama baadhi yao walivyomjaribu, wakauawa na nyoka. Wala msinungunike kama baadhi yao walivyonungunika, wakaangamizwa na Mwangamizi! Basi, mambo hayo yaliyowapata wao ni kielelezo kwa wengine, na yaliandikwa ili kutuonya sisi ambao mwisho wa nyakati unatukabili. Anayedhani amesimama imara ajihadhari asianguke. Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama. Kwa hiyo, wapenzi wangu, epeni ibada za sanamu. Naongea nanyi, watu wenye busara; jiamulieni wenyewe hayo nisemayo. Tunapomshukuru Mungu kwa kikombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo. Angalieni kwa mfano Wayahudi wenyewe: Wale wanaokula tambiko wanaungana na hiyo madhabahu. Nataka kusema nini, basi? Kwamba chakula kilichotambikiwa sanamu ni kitu zaidi ya chakula? Na hizo sanamu, je, ni kitu kweli zaidi ya sanamu? Hata kidogo! Ninachosema ni kwamba tambiko wanazotoa watu wasiomjua Mungu wanawatolea pepo, sio Mungu. Sipendi kamwe nyinyi muwe na ushirika na pepo. Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na kikombe cha pepo; hamwezi kushiriki katika Karamu ya Bwana na katika meza ya pepo. Au je, tunataka kumfanya Bwana awe na wivu? Mnadhani tuna nguvu zaidi kuliko yeye? Vitu vyote ni halali, lakini si vyote vinafaa. Vitu vyote ni halali lakini si vyote vinajenga. Mtu asitafute faida yake mwenyewe, ila faida ya mwenzake. Kuleni chochote kile kiuzwacho sokoni bila ya kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu; maana Maandiko yasema: “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.” Kama mtu ambaye si mwaamini akiwaalikeni nanyi mkakubali kwenda, basi, kuleni vyote atakavyowaandalieni bila kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu. Lakini mtu akiwaambieni: “Chakula hiki kimetambikiwa sanamu,” basi, kwa ajili ya huyo aliyewaambieni hivyo na kwa ajili ya dhamiri, msile. Nasema, “kwa ajili ya dhamiri,” si dhamiri yenu, bali dhamiri yake huyo aliyewaambieni. Mtaniuliza: “Kwa nini uhuru wangu utegemee dhamiri ya mtu mwingine? Ikiwa mimi nashiriki chakula hicho huku namshukuru Mungu, kwa nini nilaumiwe kwa chakula ambacho kwa ajili yake nimemshukuru Mungu?” Basi, chochote mfanyacho iwe ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Msiwe kikwazo kwa Wayahudi au kwa Wagiriki au kwa kanisa la Mungu. Muwe kama mimi; najaribu kuwapendeza wote kwa kila njia, bila kutafuta faida yangu mwenyewe ila faida ya wote, wapate kuokolewa. Niigeni mimi kama nami ninavyomwiga Kristo. Nawapeni hongera kwa sababu mnanikumbuka na kwa sababu mnayashikilia yale maagizo niliyowapeni. Lakini napenda pia mjue kwamba Kristo ni kichwa cha kila mwanamume, na mwanamume ni kichwa cha mkewe, na Mungu ni kichwa cha Kristo. Basi, kila mwanamume anayesali au anayetangaza ujumbe wa Mungu huku amefunika kichwa chake, huyo anamdharau Kristo. Na mwanamke akisali au kutangaza ujumbe wa Mungu bila kufunika kichwa chake, anamdharau mumewe; anayefanya hivyo ni sawa tu na mwanamke aliyenyoa kichwa chake. Mwanamke asiyefunika kichwa chake, afadhali anyoe nywele zake. Lakini ni aibu kwa mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa; basi, afadhali afunike kichwa chake. Haifai mwanamume kufunika kichwa chake, kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na kioo cha utukufu wake Mungu; lakini mwanamke ni kioo cha utukufu wa mwanamume. Mwanamume hakutoka kwa mwanamke, ila mwanamke alitoka kwa mwanamume. Mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, ila mwanamke aliumbwa kwa ajili ya mwanamume. Ndiyo maana mwanamke hufunika kichwa chake, iwe ishara ya mamlaka yaliyo juu yake, na pia kwa sababu ya malaika. Hata hivyo, mbele ya Bwana mwanamke si kitu bila mwanamume, naye mwanamume si kitu bila mwanamke. Kama vile mwanamke alivyotokana na mwanamume, vivyo hivyo mwanamume huzaliwa na mwanamke; kila kitu hutoka kwa Mungu. Amueni wenyewe: Je, inafaa mwanamke kumwomba Mungu bila kuvaa kitu kichwani? Hata maumbile yenyewe huonesha wazi kwamba kwa mwanamume kuwa na nywele ndefu ni aibu kwake mwenyewe; lakini kwa mwanamke kuwa na nywele ni heshima kwake; nywele zake ndefu amepewa ili zimfunike. Kama mtu anataka kuleta ubishi juu ya jambo hili, basi, na ajue kwamba sisi hatuna desturi nyingine, wala makanisa ya Mungu hayana desturi nyingine. Nikiwa bado nawapeni maagizo haya, siwezi hata kidogo kuwapa nyinyi hongera kuhusu haya yafuatayo: Mikutano yenu nyinyi waumini yaleta hasara zaidi kuliko faida. Awali ya yote, nasikia kwamba mnapokutana pamoja hutokea mafarakano kati yenu. Nami naamini kiasi, maana ni lazima fikira tofauti ziweko miongoni mwenu, ili wale walio thabiti wapate kutambulikana. Kweli mnakutana, lakini si kwa ajili ya kula Karamu ya Bwana! Maana mnapokula kila mmoja hukikalia chakula chake mwenyewe, hata hutokea kwamba baadhi yenu wana njaa, na wengine wamelewa! Je, hamwezi kula na kunywa nyumbani kwenu! Au je, mnalidharau kanisa la Mungu na kuwaaibisha hao wasio na kitu? Niwaambie nini? Niwasifu? La hasha! Si kuhusu jambo hili. Maana mimi nilipokea kwa Bwana yale maagizo niliyowaachieni: Kwamba, usiku ule Bwana Yesu alipotolewa, alitwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akasema: “Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa kunikumbuka.” Vivyo hivyo, baada ya kula, akatwaa kikombe cha divai, akasema: “Hiki ni kikombe cha agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu. Fanyeni hivi, kila mnapokunywa, kwa kunikumbuka.” Maana kila mnapokula mkate huu na kukinywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja. Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana. Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho; maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe. Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa. Kama tungejichunguza wenyewe vizuri hatungeadhibiwa hivyo. Lakini tunapohukumiwa na Bwana, tunafunzwa tuwe na nidhamu, ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu. Kwa hiyo, ndugu zangu, mnapokutana kula Karamu ya Bwana, kila mmoja amngoje mwenzake. Na kama kuna yeyote aliye na njaa, na ale nyumbani kwake, ili kukutana kwenu kusisababishe hukumu. Lakini, kuhusu yale mambo mengine, nitawapeni maelezo nitakapokuja. Ndugu, kuhusu vipaji vya kiroho, napenda mfahamu vizuri mambo haya: Mnajua kwamba, kabla ya kuongoka kwenu, mlitawaliwa na kupotoshwa na sanamu tupu. Basi, jueni kwamba mtu yeyote anayeongozwa na Roho wa Mungu hawezi kusema: “Yesu alaaniwe!” Hali kadhalika, mtu yeyote hawezi kusema: “Yesu ni Bwana,” asipoongozwa na Roho Mtakatifu. Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho avitoaye ni mmoja. Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana anayetumikiwa ni mmoja. Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote. Kila mtu hupewa mwangaza wa Roho kwa faida ya wote. Roho humpa mmoja ujumbe wa hekima, na mwingine ujumbe wa elimu, apendavyo Roho huyohuyo. Roho huyohuyo humpa mmoja imani, na humpa mwingine kipaji cha kuponya; humpa mmoja kipaji cha kufanya miujiza, mwingine kipaji cha kusema ujumbe wa Mungu, mwingine kipaji cha kubainisha vipaji vitokavyo kwa Roho na visivyo vya Roho; humpa mmoja kipaji cha kusema lugha ngeni, na mwingine kipaji cha kuzifafanua. Hizo zote ni kazi za Roho huyohuyo mmoja, ambaye humpa kila mtu kipaji tofauti, kama apendavyo mwenyewe. Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na viungo hivyo vyote — ingawaje ni vingi — hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia kwa Kristo. Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja. Mwili hauna kiungo kimoja tu, bali una viungo vingi. Kama mguu ungejisemea: “Kwa kuwa mimi si mkono, basi mimi si mali ya mwili,” je, ungekoma kuwa sehemu ya mwili? La hasha! Kama sikio lingejisemea: “Kwa vile mimi si jicho, basi mimi si mali ya mwili,” je, kwa hoja hiyo lingekoma kuwa sehemu ya mwili? La! Kama mwili wote ungekuwa jicho, sikio lingekuwa wapi? Na kama mwili wote ungekuwa sikio, mtu angewezaje kunusa? Lakini kama ilivyo, Mungu alizipanga sehemu hizo tofauti katika mwili kama alivyopenda. Kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Ukweli ni kwamba, sehemu za mwili ni nyingi, lakini mwili ni mmoja. Basi, jicho haliwezi kuuambia mkono: “Sikuhitaji wewe,” wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: “Siwahitaji nyinyi.” Zaidi ya hayo, inaonekana kwamba sehemu zile za mwili zinazoonekana kuwa ni dhaifu ndizo zilizo muhimu zaidi. Tena, viungo vile tunavyovifikiria kuwa havistahili heshima kubwa, ndivyo tunavyovitunza kwa uangalifu zaidi; viungo vya mwili ambavyo havionekani kuwa vizuri sana, huhifadhiwa zaidi, ambapo viungo vingine havihitaji kushughulikiwa. Mungu mwenyewe ameuweka mwili katika mpango, akakipa heshima zaidi kiungo kile kilichopungukiwa heshima, ili kusiweko na utengano katika mwili, bali viungo vyote vishughulikiane. Kama kiungo kimoja kinaumia viungo vyote huumia pamoja nacho. Kiungo kimoja kikisifiwa viungo vingine vyote hufurahi pamoja nacho. Basi, nyinyi nyote ni mwili wa Kristo; kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo. Mungu ameweka katika kanisa: Kwanza mitume, pili manabii, tatu waalimu; kisha ameweka wale wenye kipaji cha kufanya miujiza, kuponya na kusaidia; viongozi na wenye kusema lugha ngeni. Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote ni wenye kipaji cha kufanya miujiza? Je, wote ni wenye kipaji cha kuponya? Je, wote ni wenye kipaji cha kusema lugha ngeni? Je, wote hufafanua lugha? Muwe basi, na tamaa ya kupata vipaji muhimu zaidi. Nami sasa nitawaonesheni njia bora zaidi kuliko hizi zote. Hata kama nikinena lugha za watu na hata za malaika, lakini kama sina upendo mimi nimekuwa tu kama sauti ya debe tupu au kengele. Tena, naweza kuwa na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, nikafahamu siri zote na kujua kila kitu; naweza kuwa na imani yote hata nikaweza kuihamisha milima, lakini kama sina upendo mimi si kitu. Nikitoa mali yangu yote na kuwapa maskini, na tena nikiutoa mwili wangu uchomwe, kama sina upendo hiyo hainifai chochote. Mwenye upendo huvumilia, hufadhili; mwenye upendo hana wivu, hajidai, wala hajivuni. Mwenye upendo hakosi adabu, hatafuti faida yake binafsi, wala hana wepesi wa hasira; haweki kumbukumbu ya mabaya, hafurahii uovu, bali hufurahia ukweli. Mwenye upendo huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote. Upendo hauna kikomo kamwe. Kama kuna vipaji vya kutangaza ujumbe wa Mungu, hivyo vitatoweka siku moja; kama ni vipaji vya kusema lugha ngeni, vitakoma; kama kuna elimu, nayo itapita. Maana ujuzi wetu si kamili, na kipaji chetu cha kutangaza neno la Mungu si kamili. Lakini kile kilicho kikamilifu kitakapofika, vyote visivyo vikamilifu vitatoweka. Nilipokuwa mtoto mchanga nilisema kitoto, nilifahamu kitoto, nilifikiri kitoto. Lakini sasa, maadamu mimi ni mtu mzima, mambo ya kitoto nimeyaacha. Tunachoona sasa ni kama tu sura hafifu katika kioo, lakini hapo baadaye tutaona uso kwa uso. Sasa ninajua kiasi fulani tu, lakini hapo baadaye nitajua yote kikamilifu, kama vile Mungu anavyonijua mimi. Sasa yanadumu haya matatu: Imani, tumaini na upendo; lakini lililo kuu kupita yote ni upendo. Jitahidini kuwa na upendo. Vilevile fanyeni bidii ya kupata vipaji vingine vya kiroho, hasa kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu. Mwenye kunena lugha ngeni hasemi na watu bali anasema na Mungu. Yeye hunena kwa nguvu ya Roho mambo yaliyofichika. Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, husema na watu kwa ajili ya kuwajenga, kuwafariji na kuwatia moyo. Mwenye kunena lugha ngeni anajijenga mwenyewe. Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, analijenga kanisa. Basi, ningependa nyinyi nyote mseme kwa lugha ngeni lakini ningependelea hasa muwe na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, maana mtu mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni wa maana zaidi kuliko yule mwenye kusema lugha ngeni, isipokuwa tu kama yupo hapo mtu awezaye kuyafafanua hayo mambo asemayo, ili kanisa lipate kujengwa. Hivyo, ndugu zangu, kama nikija kwenu na kusema nanyi kwa lugha ngeni itawafaa nini? Haitawafaa chochote, isipokuwa tu kama nitawaelezeni ufunuo wa Mungu au ujuzi fulani au ujumbe wa Mungu au mafundisho fulani. Ndivyo ilivyo kwa vyombo visivyo na uhai vyenye kutoa sauti kama vile filimbi au kinanda. Je, mtu anawezaje kuutambua wimbo unaochezwa kama vyombo hivyo havitoi sauti waziwazi vinapopigwa? La mgambo likilia bila kufuata taratibu zake, nani atajiweka tayari kwa vita? Hali kadhalika na nyinyi, kama ulimi wenu hausemi kitu chenye kueleweka, nani ataweza kufahamu mnayosema? Maneno yenu yatapotea hewani. Zipo lugha mbalimbali ulimwenguni, na hakuna hata mojawapo isiyo na maana. Lakini ikiwa mimi sifahamu maana ya lugha asemayo mtu fulani, mimi ni mgeni kwake mtu huyo naye pia ni mgeni kwangu. Hali kadhalika na nyinyi, maadamu mna hamu ya kupata vipaji vya Roho, jitahidini hasa kujipatia vile vinavyosaidia kulijenga kanisa. Kwa hiyo, mwenye kunena lugha ngeni na aombe apate uwezo wa kuzifafanua. Maana, nikisali kwa lugha ngeni roho yangu ndiyo inayosali, lakini akili yangu hubaki bure. Nifanye nini, basi? Nitasali kwa roho yangu, nitasali pia kwa akili yangu; nitaimba kwa roho yangu, nitaimba pia kwa akili yangu. Ukimsifu Mungu kwa roho yako tu, atawezaje mtu wa kawaida aliye katika mkutano kuitikia sala yako ya shukrani kwa kusema: “Amina”, kama haelewi unachosema? Sala yako ya shukrani yaweza kweli kuwa bora, lakini huyo mwingine haitamfaidia. Namshukuru Mungu kwamba mimi nasema kwa lugha ngeni kuliko nyinyi nyote. Lakini katika mikutano ya waumini napendelea zaidi kusema maneno matano yenye kueleweka ili niwafundishe wengine, kuliko kusema maneno elfu ya lugha ngeni. Ndugu, msiwe kama watoto katika fikira zenu. Kuhusu uovu, muwe kama watoto wachanga, lakini katika kufikiri ni lazima muwe kama watu waliokomaa. Imeandikwa katika sheria: “Bwana asema hivi: ‘Kwa njia ya wenye kunena lugha ngeni, na kwa midomo ya wageni, nitasema na watu hawa, hata hivyo, hawatanisikiliza.’” Hivyo basi, kipaji cha kusema lugha ngeni ni ishara, si kwa ajili ya watu wenye imani, bali kwa ajili ya wale wasioamini; lakini kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni kwa ajili ya wale wanaoamini na si kwa ajili ya wasioamini. Basi, kanisa lote linapokutana pamoja, na wote wakaanza kusema kwa lugha ngeni, kama wakija watu wa kawaida au wasioamini, je, hawatasema kwamba nyinyi mna wazimu? Lakini, wote wakiwa wanautangaza ujumbe wa Mungu, akija mtu wa kawaida au asiyeamini, yote atakayosikia yatamhakikishia ubaya wake mwenyewe; yote atakayosikia yatamhukumu. Siri za moyo wake zitafichuliwa, naye atapiga magoti na kumwabudu Mungu akisema: “Kweli Mungu yupo pamoja nanyi.” Ndugu, tuseme nini, basi? Mnapokutana pamoja, mmoja aimbe wimbo, mwingine atoe mafundisho, mwingine awe na ufunuo kutoka kwa Mungu, mwingine atumie kipaji cha kusema kwa lugha ngeni na mwingine afafanue yanayosemwa. Yote yawe kwa ajili ya kulijenga kanisa. Wakiwapo watu wenye vipaji vya kusema kwa lugha ngeni, waseme wawili au watatu, si zaidi, tena mmojammoja; na aweko mtu wa kufafanua yanayosemwa. Lakini kama hakuna awezaye kufafanua, basi, mwenye kusema lugha ngeni anyamaze mkutanoni, aseme na nafsi yake mwenyewe na Mungu. Kuhusu wale wenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, waseme wawili au watatu, na wengine wayapime maneno yao. Ikiwa mmoja anaposema na mwingine wa wasikilizaji amepata ufunuo kutoka kwa Mungu, basi, yule anayesema anyamaze. Maana nyote mwaweza kutangaza ujumbe wa Mungu, mmoja baada ya mwingine, ili nyote mpate kujifunza na kutiwa moyo. Kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni lazima kitawaliwe na huyo mwenye hicho kipaji. Maana Mungu si Mungu wa fujo, ila wa amani. Kama ilivyo desturi katika makanisa yote ya watu wa Mungu, wanawake wakae kimya katika mikutano ya waumini. Hawana ruhusa kusema; ila wawe watii kama isemavyo sheria. Ikiwa wanayo maswali ya kuuliza, wawaulize waume zao nyumbani, maana ni aibu kwa mwanamke kusema katika mikutano ya waumini. Je, mnadhani neno la Mungu limetoka kwenu nyinyi au kwamba limewajieni nyinyi peke yenu? Kama mtu yeyote anadhani kwamba yeye ni mjumbe wa Mungu au kwamba anacho kipaji cha Roho, na ajue kwamba haya ninayowaandikia nyinyi ni amri ya Bwana. Lakini mtu asiyetambua hayo, basi, mtu asimjali mtu huyo. Hivyo basi, ndugu zangu, mnapaswa kuwa na hamu ya kutangaza ujumbe wa Mungu; lakini msimkataze mtu kusema kwa lugha ngeni. Lakini yote yafanyike kwa heshima na kwa utaratibu. Sasa, ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema niliyowahubirieni, nanyi mkaipokea na kusimama imara ndani yake. Kwa njia yake mnaokolewa, ikiwa mnayazingatia maneno niliyowahubirieni, na kama kuamini kwenu hakukuwa bure. Mimi niliwakabidhi nyinyi mambo muhimu sana ambayo mimi niliyapokea: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na Maandiko Matakatifu; kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kufuatana na Maandiko Matakatifu; kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili. Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya 500 kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa. Baadaye alimtokea Yakobo kisha akawatokea mitume wote. Baada ya wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama mtu aliyezaliwa kabla ya wakati. Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume, na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu. Lakini, kwa neema yake Mungu, nimekuwa kama nilivyo, na neema yake kwangu haikuwa bure. Mimi nimefanya kazi kuliko wote; si mimi hasa, ila ni neema ya Mungu ifanyayo kazi pamoja nami. Lakini hata hivyo, iwe wao ndio wahubirio au mimi nihubiriye, haidhuru, hiki ndicho tunachohubiri, na hiki ndicho mnachoamini. Sasa, maadamu inahubiriwa kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, baadhi yenu wanawezaje kusema kwamba hakuna ufufuo wa wafu? Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka; na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yenu haina maana. Zaidi ya hayo sisi tungekuwa mashahidi wa uongo mbele ya Mungu, maana tulisema kwamba Mungu alimfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumbe yeye hakumfufua — kama ni kweli kwamba wafu hawafufuliwi. Maana, ikiwa ni kweli kwamba wafu hawafufuki, basi naye Kristo hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuliwa, basi, imani yenu ni ya bure; mngali bado katika dhambi zenu. Zaidi ya hayo, wale wote waliokufa wakiwa wameungana na Kristo wamepotea kabisa. Kama matumaini yetu katika Kristo yanahusu tu maisha haya ya sasa, basi, sisi ni watu wa kusikitikiwa zaidi kuliko wengine wote duniani. Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, wa kwanza wa wale waliolala katika kifo. Maana kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo hivyo nako kufufuka kutoka kwa wafu kumesababishwa na mtu mmoja. Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo. Lakini kila mmoja kwa mpango wake: Kristo kwanza; halafu wale walio wake Kristo wakati Kristo atakapokuja. Baada ya hayo, mwisho utafika wakati ambapo Kristo atamkabidhi Mungu Baba ufalme, baada ya kufutilia mbali kila tawala na mamlaka na nguvu. Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda maadui zake wote na kuwaweka chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo. Maana, Maandiko yasema: “Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini, Maandiko yanaposema: “Vitu vyote vimewekwa chini ya miguu yake avitawale” ni dhahiri kwamba Mungu haingii katika kundi hilo la vitu, maana yeye ndiye anayeviweka vitu hivyo chini ya Kristo. Lakini vitu vyote vitakapowekwa chini ya utawala wa Kristo, ndipo naye Mwana atakapojiweka chini ya Mungu, aliyeweka vyote chini ya utawala wake; ili Mungu atawale juu ya vyote. Kama hakuna ufufuo, je watu wale wanaobatizwa kwa ajili ya wafu wanatumainia kupata nini? Kama wafu hawafufuliwi, ya nini kubatizwa kwa ajili yao? Na sisi, ya nini kujitia hatarini kila saa? Ndugu, mimi nakikabili kifo kila siku! Fahari niliyo nayo juu yenu katika kuungana na Kristo Yesu Bwana wetu inanifanya nitangaze jambo hili. Kama kusudi langu lingalikuwa la kibinadamu tu, kule kupigana kwangu na wanyama wakali hapa Efeso kungalinifaa kitu gani? Kama wafu hawafufuki, basi, “Tule na tunywe, maana kesho tutakufa.” Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema. Amkeni! Anzeni kuishi vema, na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hawamjui Mungu kabisa. Hii nawaambieni, ni aibu kubwa kwenu! Lakini mtu anaweza kuuliza: “Wafu watafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” Hayo ni maswali ya kijinga! Ukipanda mbegu, isipokufa kwanza haitaota. Unachopanda ni mbegu tu, labda ya ngano au nafaka nyingine, na si mmea mzima ambao hutokea baadaye. Mungu huipa hiyo mbegu mwili anaoutaka mwenyewe; kila mbegu hupata mwili wake wa pekee. Miili ya viumbe vyote si sawa. Miili ya binadamu ni ya namna moja, ya wanyama ni ya namna nyingine, ya ndege ni ya namna nyingine na miili ya samaki pia ni ya namna nyingine. Iko miili ya mbinguni na miili ya duniani; uzuri wa miili ya mbinguni ni mwingine, na uzuri wa miili ya duniani ni mwingine. Uko uzuri wa jua, wa mwezi na wa nyota; hata nyota nazo huhitilafiana kwa uzuri. Ndivyo ilivyo kuhusu ufufuo wa wafu. Kama vile mbegu, mwili huzikwa ardhini ukiwa katika hali ya kuharibika, lakini hufufuliwa katika hali ya kutoharibika. Huzikwa katika hali duni, hufufuliwa katika hali tukufu; huzikwa katika hali dhaifu, hufufuliwa ukiwa wenye nguvu. Unapozikwa ni mwili wa kawaida, unapofufuliwa ni mwili wa kiroho. Kuna mwili wa kawaida na kutakuwa na mwili wa kiroho. Maana Maandiko yasema: “Mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe mwenye uhai;” lakini Adamu wa mwisho ni Roho awapaye watu uhai. Lakini unaotangulia kuwako si ule mwili wa kiroho, ila ule mwili wa kawaida, kisha ule mwili wa kiroho. Adamu wa kwanza aliumbwa kwa udongo, alitoka ardhini; mtu wa pili alitoka mbinguni. Wote walio wa dunia wako kama huyo mtu aliyeumbwa kwa udongo; wale walio wa mbinguni wako kama yule aliyetoka mbinguni. Kama vile tulivyofanana na yule aliyeumbwa kwa udongo, vivyo hivyo tutafanana na huyo aliyetoka mbinguni. Basi, ndugu, nasema hivi: Kile kilichofanywa kwa mwili na damu hakiwezi kuushiriki ufalme wa Mungu; na chenye kuharibika hakiwezi kuwa na hali ya kutoharibika. Sikilizeni, nawaambieni siri: Sisi hatutakufa sote, ila sote tutageuzwa, wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na kufumbua. Maana tarumbeta ya mwisho itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutoweza kufa tena, na sisi tutageuzwa. Maana ni lazima kila kiharibikacho kijivalie hali ya kutoharibika, mwili uwezao kufa ujivalie hali ya kutokufa. Basi, mwili huu wenye kuharibika utakapojivalia hali ya kutoharibika, na kile chenye kufa kitakapojivalia hali ya kutokufa, hapo ndipo litakapotimia lile neno lililoandikwa: “Kifo kimeangamizwa; ushindi umekamilika!” “Kifo, ushindi wako uko wapi? Uwezo wako wa kuumiza uko wapi?” Kifo hupata sumu yake katika dhambi, nayo dhambi hupata nguvu yake katika sheria. Lakini tumshukuru Mungu anayetupatia ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu zangu wapenzi, simameni imara na thabiti. Endeleeni daima kuwa na bidii katika kazi ya Bwana, mkijua kwamba kazi mnayofanya katika utumishi wa Bwana haitapotea bure. Sasa, yahusu ule mchango kwa ajili ya watu wa Mungu: Fanyeni kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia. Kila Jumapili kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha kadiri ya mapato yake, ili kusiwe na haja ya kufanya mchango wakati nitakapokuja. Wakati nitakapokuja kwenu, nitawatuma wale mtakaowachagua miongoni mwenu wapeleke barua na zawadi zenu Yerusalemu. Kama itafaa nami niende, basi, watakwenda pamoja nami. Nitakuja kwenu baada ya kupitia Makedonia — maana nataraji kupitia Makedonia. Labda nitakaa kwenu kwa muda fulani, au huenda nitakaa pamoja nanyi wakati wote wa baridi, ili mpate kunisaidia niendelee na safari yangu kokote nitakakokwenda. Sipendi kupita kwenu harakaharaka na kuendelea na safari. Natumaini kukaa kwenu kwa kitambo fulani, Bwana akiniruhusu. Lakini nitabaki hapa Efeso mpaka siku ya Pentekoste. Mlango uko wazi kabisa kwa ajili ya kazi yangu muhimu hapa, ingawa wapinzani nao ni wengi. Timotheo akija, angalieni asiwe na hofu yoyote wakati yupo kati yenu, kwani anafanya kazi ya Bwana kama mimi. Kwa hiyo mtu yeyote asimdharau, ila msaidieni aendelee na safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu, maana mimi namngojea pamoja na ndugu zetu. Kuhusu ndugu Apolo, nimemsihi sana aje kwenu pamoja na ndugu wengine, lakini hapendelei kabisa kuja sasa ila atakuja mara itakapowezekana. Kesheni, simameni imara katika imani, muwe hodari na wenye nguvu. Kila mfanyacho kifanyike kwa upendo. Ndugu, mnaifahamu jamaa ya Stefana; wao ni watu wa kwanza kabisa kuipokea imani ya Kikristo katika Akaya, na wamejitolea kuwatumikia watu wa Mungu. Ninawasihi nyinyi ndugu zangu, muufuate uongozi wa watu kama hao, na uongozi wa kila mtu afanyaye kazi na kutumika pamoja nao. Nafurahi sana kwamba Stefana, Fortunato na Akaiko wamefika; wamelijaza pengo lililokuwako kwa kutokuwako kwenu. Wameiburudisha roho yangu na yenu pia. Kwa hiyo inafaa kuwakumbuka watu wa namna hii. Makanisa yote ya Asia yanawasalimuni. Akula na Priska pamoja na watu wote wa Mungu walio nyumbani mwao wanawasalimuni sana katika kuungana na Bwana. Ndugu wote wanawasalimuni. Nanyi salimianeni kwa ishara ya mapendo ya Mungu. Mimi Paulo nawasalimuni, nikiandika kwa mkono wangu mwenyewe. Yeyote asiyempenda Bwana, na alaaniwe. MARANATHA — BWANA, NJOO! Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi. Upendo wangu uwe kwenu katika kuungana na Kristo Yesu. Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia nyinyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho, na watu wote wa Mungu kila mahali katika Akaya. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo. Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu. Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye. Ikiwa tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni kwa ajili ya kuwafariji nyinyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili mateso yaleyale tunayoteseka sisi. Tena, matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu. Ndugu, tunataka kuwajulisheni taabu zilizotupata kule Asia; taabu hizo zilitulemea kupita kiasi, hata tukakata matumaini yote ya kuendelea kuishi. Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe. Yeye alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea tumaini letu kwamba atatuokoa tena, nyinyi mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu kwa ajili yetu. Sisi tunajivunia kitu kimoja: Dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali na neema ya Mungu. Tunawaandikia nyinyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa, maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea nyinyi fahari. Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu. Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea. Je, mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema “Ndiyo” na “Siyo” papo hapo? Mungu ni ukweli tupu; basi, kile tulichowaambia nyinyi si jambo la “Ndiyo” na “Siyo”. Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa “Ndiyo” na “Siyo;” bali yeye daima ni “Ndiyo” ya Mungu. Maana ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa “Ndiyo”. Kwa sababu hiyo, “Amina” yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu. Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na nyinyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu; ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea. Mungu ndiye shahidi wangu; yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho kwa sababu tu ya kuwahurumieni. Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; nyinyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu. Basi, nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni. Maana nikiwahuzunisha nyinyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha! Ndiyo maana niliwaandikia: Sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na nyinyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba mimi nikifurahi, nyinyi nyote pia mnafurahi. Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha nyinyi, bali kwa ajili ya kuwaonesheni kwamba nawapenda mno. Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi, ila amewahuzunisha nyinyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi. Adhabu aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha. Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa. Kwa hiyo nawasihi: Mwonesheni kwamba mnampenda. Madhumuni yangu ya kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo. Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe, kama kweli ninacho cha kusamehe, nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo. Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana. Lakini nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia. Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali. Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote, wanaookolewa na wanaopotea. Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo? Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo. Je, tunaanza tena kujipendekeza? Je, tunahitaji barua ya utambulisho kwenu, au kutoka kwenu, kama watu wengine? Nyinyi wenyewe ni barua yetu; barua iliyoandikwa mioyoni mwetu kila mtu aione na kuisoma. Ni dhahiri kwamba nyinyi ni barua ya Kristo aliyoipeleka kwa mikono yetu. Barua yenyewe imeandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; imeandikwa si juu ya kipande cha jiwe, bali juu ya mioyo ya watu. Tunaweza kusema hayo kwa sababu ya tumaini letu tulilo nalo kwa Mungu kwa njia ya Kristo. Si kwamba sisi tunaweza kufanya chochote kwa nguvu zetu wenyewe, ila uwezo wetu wote hutoka kwa Mungu: Maana yeye ndiye aliyetuwezesha kulihudumia Agano Jipya ambalo si agano la sheria iliyoandikwa, bali agano la Roho. Maana sheria iliyoandikwa huleta kifo, lakini Roho huleta uhai. Sheria iliwekwa kwa kuandikwa juu ya vipande vya mawe. Ingawaje mwisho wake umekuwa kifo, utukufu wake ulikuwa mkuu mno hata wana wa Israeli wasiweze kuutazama uso wa Mose kwa sababu ya mngao wake. Tena mngao huo ulikuwa wa muda tu. Basi, ikiwa huduma ya kile ambacho kimesababisha kifo imefanyika kwa utukufu mwingi kiasi hicho, basi, huduma ya Roho ina utukufu mkuu zaidi. Ikiwa basi, kulikuwa na utukufu katika huduma ile iliyoleta hukumu, ni wazi kwamba huduma iletayo uadilifu itakuwa na utukufu mkuu zaidi. Sasa utukufu mkuu zaidi umechukua nafasi ya ule utukufu uliokuja hapo awali, ambao fahari yake imekwisha toweka. Maana ikiwa kile kilichokuwa cha muda tu kilikuwa na utukufu wake, bila shaka kile chenye kudumu milele kitakuwa na utukufu mkuu zaidi. Kwa vile hili ndilo tumaini letu, sisi twasema kwa uhodari mkuu. Sisi hatufanyi kama Mose ambaye alilazimika kuufunika uso wake kwa kitambaa ili watu wa Israeli wasiuone ule mwisho wa mngao ule uliokuwa unafifia. Lakini akili zao zilipumbazwa. Mpaka leo hii lisomwapo Agano la Kale, kifuniko hicho bado kipo. Kifuniko hicho kitaondolewa tu mtu anapoungana na Kristo. Naam, mpaka hivi leo kila isomwapo sheria akili zao huwa zimefunikwa. Lakini, wakati mtu amgeukiapo Bwana, kifuniko hicho huondolewa. Hapa “Bwana” ni Roho; na pale alipo Roho wa Bwana ndipo ulipo uhuru. Basi, sisi sote ambao nyuso zetu hazikufunikwa, tunaona kama katika kioo, utukufu wa Bwana; tunabadilishwa tufanane zaidi na huo mfano wake kwa utukufu mwingi zaidi. Hiyo ni kazi yake Roho wa Bwana. Basi, Mungu, kwa huruma yake, ametukabidhi kazi hii na hivyo hatufi moyo. Tumeyaacha kabisa mambo yote ya aibu na ya kisirisiri. Hatuishi tena kwa udanganyifu, wala kwa kulipotosha neno la Mungu; bali kwa kuudhihirisha ukweli twajiweka chini ya uamuzi wa dhamiri za watu mbele ya Mungu. Maana, kama Habari Njema tunayohubiri imefichika, imefichika tu kwa wale wanaopotea. Hao hawaamini kwa sababu yule mungu wa ulimwengu huu amezitia giza akili zao wasipate kuuona wazi mwanga wa Habari Njema ya utukufu wa Kristo, ambaye ni mfano kamili wa Mungu. Maana hatujitangazi sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo aliye Bwana, sisi wenyewe tukiwa watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. Mungu ambaye alisema, “Mwanga na uangaze kutoka gizani,” ndiye mwenye kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao katika uso wa Kristo. Basi, sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe. Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa; twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa. Kila wakati tumekuwa tukichukua mwilini mwetu kifo cha Kristo, ili uhai wake Yesu pia udhihirike katika miili yetu. Naam, muda tuishipo tunakabiliwa na kifo daima kwa ajili ya Yesu, ili uhai wake Yesu udhihirike katika miili yetu inayokufa. Hii ina maana kwamba ndani yetu kifo kinafanya kazi, lakini ndani yenu uhai unafanya kazi. Maandiko Matakatifu yasema: “Niliamini, ndiyo maana nilinena.” Nasi pia, tukiwa na moyo huohuo wa imani, tunaamini, na kwa sababu hiyo twanena. Tunajua kwamba yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka mbele yake pamoja nanyi. Yote haya ni kwa faida yenu, hata neema ya Mungu inapowafikia watu wengi zaidi na zaidi, shukrani nazo ziongezeke zaidi, kwa utukufu wa Mungu. Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku. Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu; lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho. Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele. Maana tunajua kwamba hema hii ambamo tunaishi sasa hapa duniani yaani mwili wetu, itakapongolewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono. Na sasa, katika hali hii, tunaugua tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni. Naam, tunapaswa kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi. Tukiwa bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile chenye kufa kimezwe kabisa na uhai. Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea. Tuko imara daima. Tunajua kwamba kuishi katika mwili huu tu ni kukaa mbali na Bwana. Maana tunaishi kwa imani, na si kwa kuona. Lakini tuko imara na tungependelea hata kuyahama makao haya, tukahamie kwa Bwana. Lakini jambo la maana zaidi, tunataka kumpendeza, iwe tunaishi hapa duniani au huko. Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya. Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga. Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa nyinyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni. Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu. Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake. Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao. Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu. Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena. Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika. Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo, na kutupa jukumu la kuwapatanisha watu naye. Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye. Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi nyinyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki uadilifu wake Mungu. Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure. Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia.” Basi, sasa ndio wakati wa kufaa; sasa ndiyo siku ya wokovu! Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuizi chochote. Badala yake, tunajionesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: Kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu. Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula. Tunajionesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki, kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu kila upande. Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli; kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote; kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni hai kabisa. Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini, twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu. Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa. Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu nyinyi wenyewe, na si kwa upande wetu. Sasa nasema nanyi kama watoto wangu: Wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya. Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja? Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Mwaamini ana uhusiano gani na asiyeamini? Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema: “Nitafanya makao yangu kwao, na kuishi kati yao. Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” Kwa hiyo Bwana asema pia: “Ondokeni kati yao, mkajitenge nao; msiguse kitu najisi, nami nitawapokea. Mimi nitakuwa Baba yenu, nanyi mtakuwa wanangu, waume kwa wake, asema Bwana Mwenye Nguvu.” Basi, wapenzi wangu, tukiwa tumepewa ahadi hizi zote, na tujitakase na chochote kiwezacho kuchafua miili na roho zetu, tuwe watakatifu kabisa na kuishi kwa kumcha Mungu. Tunaomba mtupe nafasi mioyoni mwenu! Hatujamkosea mtu yeyote, hatujamdhuru wala kumdanganya mtu yeyote. Sisemi mambo haya kwa ajili ya kumhukumu mtu; maana, kama nilivyokwisha sema, nyinyi mko mioyoni mwetu, tufe pamoja, tuishi pamoja. Nina imani kubwa sana ninaposema nanyi; naona fahari kubwa juu yenu! Katika taabu zetu nimepata kitulizo kikubwa na kufurahi mno. Hata baada ya kufika Makedonia hatukuweza kupumzika. Kila upande tulikabiliwa na taabu: Nje ugomvi; ndani hofu. Lakini Mungu, mwenye kuwapa shime wanyonge, alitupa moyo sisi pia kwa kuja kwake Tito. Si tu kwa kule kuja kwake Tito, bali pia kwa sababu ya moyo mliompa nyinyi. Yeye ametuarifu jinsi mnavyotamani kuniona, jinsi mlivyo na huzuni, na mnavyotaka kunitetea. Jambo hili linanifurahisha sana. Maana, hata kama kwa barua yangu ile nimewahuzunisha, sioni sababu ya kujuta. Naam, naona kwamba barua hiyo iliwatia huzuni lakini kwa muda. Sasa nafurahi, si kwa sababu mmehuzunika, ila kwa kuwa huzuni yenu imewafanya mbadili nia zenu na kutubu. Mmehuzunishwa kadiri ya mpango wa Mungu, na kwa sababu hiyo hatukuwadhuru nyinyi kwa vyovyote. Kuwa na huzuni jinsi atakavyo Mungu husababisha badiliko la moyo, badiliko lenye kuleta wokovu; hivyo hakuna sababu ya kujuta. Lakini huzuni ya kidunia huleta kifo. Sasa mnaweza kuona matokeo ya kuona huzuni jinsi Mungu atakavyo: Nyinyi mmepata kuwa sasa watu wenye jitihada, wenye hoja, mnashtuka na kuogopa, mna bidii na mko tayari kuona kwamba haki yatekelezwa. Nyinyi mmethibitisha kwa kila njia kwamba hamna hatia kuhusu jambo hili. Hivyo, ingawa niliandika ile barua, haikuwa kwa ajili ya yule aliyekosa, au kwa ajili ya yule aliyekosewa. Niliandika kusudi ionekane wazi mbele ya Mungu jinsi mlivyo na bidii kwa ajili yetu. Ndiyo maana sisi tulifarijika sana. Siyo kwamba tulifarijika tu, ila pia Tito alitufurahisha kwa furaha aliyokuwa nayo kutokana na jinsi mlivyomchangamsha moyo. Mimi nimewasifu sana mbele yake, na katika jambo hilo sikudanganyika. Tumewaambieni ukweli daima, na kule kuwasifia nyinyi mbele ya Tito kumekuwa jambo la ukweli tupu. Hivyo upendo wake wa moyo kwenu nyinyi unaongezeka zaidi akikumbuka jinsi nyinyi nyote mlivyo tayari kutii, na jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu nyingi na kutetemeka. Nafurahi sana kwamba naweza kuwategemea nyinyi kabisa katika kila jambo. Ndugu, tunapenda kuwapa habari juu ya neema ambazo Mungu ameyajalia makanisa ya Makedonia. Waumini wa huko walijaribiwa sana kwa taabu; lakini furaha yao ilikuwa kubwa hivi hata wakawa wakarimu kupita kiasi, ingawaje walikuwa maskini sana. Naweza kushuhudia kwamba walikuwa wakarimu kadiri ya nguvu zao na hata zaidi. Kwa hiari yao wenyewe, walitusihi sana wapewe nafasi ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watu wa Mungu. Hilo lilikuwa jambo ambalo hatukulitazamia kabisa! Kwanza walijitolea wao wenyewe kwa Bwana, kisha wakajitolea wenyewe kwetu pia, kufuatana na mapenzi ya Mungu. Kwa sababu hiyo, tulimsihi Tito aliyeianza kazi hiyo awasaidieni pia mwitekeleze huduma hii ya upendo miongoni mwenu. Nyinyi mna kila kitu: Imani, uwezo wa kusema, elimu; bidii yote ya kutenda mema, na upendo wenu kwetu. Hivyo, tunatazamia muwe wakarimu katika huduma hii ya upendo. Siwapi nyinyi amri, lakini nataka tu kuonesha jinsi wengine walivyo na bidii ya kusaidia ili nipate kujua jinsi upendo wenu ulivyo wa kweli. Maana, nyinyi mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo: Yeye, ingawa alikuwa na kila kitu, alijifanya maskini kwa ajili yenu, ili kutokana na umaskini wake, awatajirishe. Kuhusu jambo hili, basi, nawapeni shauri hili: Inafaa kwenu kutekeleza sasa yale mliyoanza mwaka jana. Nyinyi mlikuwa wa kwanza kuchukua hatua na kuamua kufanya hivyo. Basi, kamilisheni shughuli hiyo; na kama vile mlivyokuwa na hamu kubwa ya kusaidia, basi, fanyeni bidii vivyo hivyo, kadiri ya uwezo wenu, kuikamilisha. Maana ikiwa mtu ana moyo wa kusaidia, Mungu hupokea kila anachoweza kutoa; hadai zaidi. Nyinyi hampaswi kuongezewa taabu kusudi wengine wapunguziwe mzigo wao; sivyo, ila ni lazima tujali usawa na haki. Kila mlicho nacho sasa cha ziada kiwasaidie wale wanaohitaji, ili nao wakati watakapokuwa na ziada, wawasaidie nyinyi katika mahitaji yenu, na hivyo kuwe na usawa. Kama Maandiko yasemavyo: “Aliyekusanya kwa wingi hakuwa na ziada, na yule aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.” Namshukuru Mungu aliyeweka ndani ya moyo wa Tito hamu hiyo niliyo nayo mimi ya kuwasaidia. Si tu kwamba alikubali ombi letu, ila pia alikuwa na hamu kubwa ya kusaidia, hata akaamua kwa hiari yake mwenyewe kuja kwenu. Pamoja naye, tunamtuma ndugu mmoja ambaye sifa zake katika kueneza Injili zimeenea katika makanisa yote. Zaidi ya hayo, yeye amechaguliwa na makanisa awe mwenzetu safarini wakati tunapopeleka huduma hii yetu ya upendo, huduma tunayoifanya kwa ajili ya utukufu wa Bwana na uthibitisho wa nia yetu njema. Tunataka kuepa lawama zinazoweza kutokea kuhusu usimamizi wetu juu ya zawadi hii karimu. Nia yetu ni kufanya vema, si mbele ya Bwana tu, lakini pia mbele ya watu. Basi, pamoja na ndugu hao, tumemtuma ndugu yetu mwingine ambaye mara nyingi tumempa majaribio mbalimbali, tukamwona kuwa ni mwenye hamu kubwa ya kusaidia; hata sasa amekuwa na moyo zaidi kwa sababu ana imani sana nanyi. Tito ni mwenzangu; tunafanya kazi pamoja kwa ajili yenu; lakini kuhusu hawa ndugu zetu wengine wanaokuja pamoja nao, hao ni wajumbe wa makanisa, utukufu kwa Kristo. Basi, waonesheni uthabiti wa upendo wenu, makanisa yapate kuona kweli kwamba fahari ninayoona juu yenu ni ya halali. Si lazima kuandika zaidi kuhusu huduma yenu hiyo kwa ajili ya watu wa Mungu. Ninajua jinsi mlivyo na moyo wa kusaidia, na nilijivuna juu yenu kuhusu jambo hilo mbele ya watu wa Makedonia. Niliwaambia: “Ndugu zetu wa Akaya wako tayari tangu mwaka jana.” Hivyo, moto wenu umekwisha wahimiza watu wengi zaidi. Basi, nimewatuma ndugu zetu hao, ili fahari yetu juu yenu ionekane kwamba si maneno matupu, na kwamba mko tayari kabisa na msaada wenu kama nilivyosema. Isije ikawa kwamba watu wa Makedonia watakapokuja pamoja nami tukawakuta hamko tayari, hapo sisi tutaaibika — bila kutaja aibu mtakayopata nyinyi wenyewe — kwa sababu tutakuwa tumewatumainia kupita kiasi. Kwa hiyo, nimeona ni lazima kuwaomba hawa ndugu watutangulie kuja kwenu, wapate kuweka tayari zawadi yenu kubwa mliyoahidi; nayo ioneshe kweli kwamba ni zawadi iliyotolewa kwa hiari na si kwa kulazimishwa. Kumbukeni: “Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi.” Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha. Mungu anaweza kuwapeni nyinyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Yeye hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini; wema wake wadumu milele.” Na Mungu ampaye mkulima mbegu na mkate kwa chakula, atawapa nyinyi pia mbegu mnazohitaji, na atazifanya ziote, zikue na kuwapa mavuno mengi ya ukarimu wenu. Yeye atawatajirisha nyinyi daima kwa kila kitu, ili watu wapate kumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi zenu wanazozipokea kwa mikono yetu. Maana huduma hii takatifu mnayoifanya si kwamba itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu tu, bali pia itasababisha watu wengi wamshukuru Mungu. Kutokana na uthibitisho unaooneshwa kwa huduma hii yetu, watu watamtukuza Mungu kwa sababu ya uaminifu wenu kwa Habari Njema ya Kristo mnayoiungama, na pia kwa sababu ya ukarimu mnaowapa wao na watu wote. Kwa hiyo watawaombea nyinyi kwa moyo kwa sababu ya neema ya pekee aliyowajalieni Mungu. Tumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi yake isiyo na kifani! Mimi Paulo mwenyewe ambaye naonekana kuwa mpole nikiwa pamoja nanyi, lakini mkali niwapo mbali nanyi, nawasihini kwa huruma na wema wake Kristo. Nawaombeni msinisababishe kuwa mkali wakati nitakapokuja, maana nina hakika naweza kuwa mkali kwa wote wale wanaotudhania kwamba tunaishi kidunia. Kweli tunaishi duniani, lakini hatupigani vita kidunia. Maana, silaha tunazotumia katika vita vyetu si silaha za kidunia, ila ni nguvu ya Mungu yenye kuharibu ngome zote. Tunaharibu hoja zote za uongo na kubomoa kila kizuizi cha majivuno kilichowekwa kuipinga elimu ya Mungu; tunaziteka fikira zote na kuzifanya zimtii Kristo. Mkisha kuwa wakamilifu katika kutii, sisi tuko tayari kuadhibu kila namna ya kutotii. Nyinyi hutazama mambo kwa nje tu. Je, yupo mtu yeyote anayedhani kwamba yeye ni wa Kristo? Sawa! Basi, afikirie vilevile kwamba sisi pia ni wa Kristo kama yeye alivyo wa Kristo. Hata kama nimezidi katika kujivuna kwangu juu ya ule uwezo aliotupa — uwezo wa kuwajenga na sio wa kubomoa — hata hivyo sijuti hata kidogo. Sipendi mfikiri kwamba nataka kuwatisha nyinyi kwa barua zangu. Mtu anaweza kusema: “Barua za Paulo ni kali na zenye maneno mazito, lakini yeye mwenyewe anapokuwa pamoja nasi ni mtu dhaifu, na hata anapoongea maneno yake ni kama si kitu.” Mtu asemaye hivyo heri akumbuke kwamba hakuna tofauti ya yale tunayoandika katika barua wakati tuko mbali, na yale tutakayofanya wakati tutakapokuwa nanyi. Kwa vyovyote hatungethubutu kujiweka au kujilinganisha na wale watu wanaojisifia wenyewe. Watu wenye kujifanya wao kuwa kipimo cha kujipimia, na watu wanaojilinganisha wenyewe kwa wenyewe, ni wapumbavu. Lakini sisi hatutajivuna kupita kiasi; kujivuna huko kutabaki katika kile kipimo cha kazi aliyotukabidhi Mungu, kazi ambayo tunaifanya pia kwenu. Hatukuruka mipaka tuliyowekewa wakati tulipokuja kwenu. Sisi tulikuwa wa kwanza kuja kwenu tukiwaleteeni Habari Njema juu ya Kristo. Basi, hatujivunii kazi waliyofanya wengine zaidi ya kipimo tulichopewa; ila tunatumaini kwamba imani yenu itazidi miongoni mwenu kufuatana na kipimo alichotuwekea Mungu. Hapo tutaweza kuihubiri Habari Njema katika nchi nyingine, mbali nanyi; na haitakuwa shauri la kujivunia kazi waliyofanya watu wengine mahali pengine. Lakini kama yasemavyo Maandiko: “Mwenye kujivuna na ajivunie kazi ya Bwana.” Anayekubaliwa si yule anayejisifu mwenyewe, bali yule anayesifiwa na Bwana. Laiti mngenivumilia kidogo, hata kama mimi ni mjinga kiasi! Naam, nivumilieni kidogo. Ninawaoneeni wivu lakini ni wivu wa Mungu; maana nyinyi ni kama bikira safi niliyemposa kwa mwanamume mmoja tu ambaye ndiye Kristo. Lakini naogopa kwamba, kama vile yule nyoka kwa hila zake za uongo alimdanganya Hawa, fikira zenu zaweza kupotoshwa, mkauacha uaminifu wenu wa kweli kwa Kristo. Maana mtu yeyote ajaye na kumhubiri Yesu aliye tofauti na yule tuliyemhubiri, nyinyi mwampokea kwa mikono miwili; au mnakubali roho au Injili tofauti kabisa na ile mliyopokea kutoka kwetu! Sidhani kwamba mimi ni mdogo kuliko hao “mitume wakuu.” Labda sina ufasaha wa lugha, lakini elimu ninayo; jambo hili tumelionesha wazi kwenu, kila mahali na kila wakati. Mimi niliihubiri kwenu Habari Njema ya Mungu bila kudai mshahara; nilijinyenyekesha ili nipate kuwakweza nyinyi. Je, nilifanya vibaya? Nilipofanya kazi kati yenu, mahitaji yangu yaligharimiwa na makanisa mengine. Kwa namna moja au nyingine niliwapokonya wao mali yao nipate kuwatumikia nyinyi. Nilipokuwa nanyi sikumsumbua mtu yeyote nilipohitaji fedha; ndugu waliotoka Makedonia waliniletea kila kitu nilichohitaji. Nilikuwa mwangalifu sana nisiwe mzigo kwa namna yoyote ile, na nitaendelea kufanya hivyo. Naahidi kwa ule ukweli wa Kristo ulio ndani yangu, kwamba hakuna kitakachoweza kunizuia kujivunia jambo hilo popote katika Akaya. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu eti siwapendi nyinyi? Mungu anajua kwamba nawapenda! Nitaendelea kufanya kama ninavyofanya sasa, ili nisiwape nafasi wale wanaotafuta nafasi, nafasi ya kujivuna kwamba eti wanafanya kazi kama sisi. Maana, hao ni mitume wa uongo, wafanyakazi wadanganyifu wanaojisingizia kuwa mitume wa Kristo. Wala si ajabu, maana hata Shetani mwenyewe hujisingizia kuwa malaika wa mwanga! Kwa hiyo si jambo la kushangaza ikiwa na hao watumishi wake wanajisingizia kuwa watumishi wa haki. Mwisho wao watapata kile wanachostahili kufuatana na matendo yao. Tena nasema: Mtu asinifikirie kuwa mpumbavu. Lakini kama mkifikiri hivyo, basi, nichukueni kama mpumbavu ili nami nipate kuwa na cha kujivunia angaa kidogo. Ninachosema sasa si kile alichoniagiza Bwana; kuhusu jambo hili la kujivuna, nasema tu kama mtu mpumbavu. Maadamu wengi hujivuna kwa sababu za kidunia, nami pia nitajivuna. Nyinyi ni wenye busara, ndiyo maana hata mnawavumilia wapumbavu! Mnamvumilia hata mtu anayewafanya nyinyi watumwa, mtu mwenye kuwanyonya, mwenye kuwakandamiza, mwenye kuwadharau na kuwapiga usoni! Kwa aibu nakubali kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Iwe iwavyo, lakini kama kuna mtu yeyote anayethubutu kujivunia kitu — nasema kama mtu mpumbavu — mimi nathubutu pia. Je, wao ni Waebrania? Hata mimi. Je, wao ni Waisraeli? Hata mimi. Wao ni wazawa wa Abrahamu? Hata mimi. Wao ni watumishi wa Kristo? Hata mimi — nanena hayo kiwazimu — ni mtumishi wa Kristo zaidi kuliko wao. Mimi nimefanya kazi ngumu zaidi, nimekaa gerezani mara nyingi zaidi, nimepigwa mara nyingi zaidi na nimekaribia kifo mara nyingi. Mara tano nilichapwa vile viboko arubaini kasoro kimoja vya Wayahudi. Nilipigwa fimbo mara tatu, nilipigwa mawe mara moja; mara tatu nilivunjikiwa meli baharini, na humo nikakesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa. Kila mara safarini nimekabiliwa na hatari za mafuriko ya mito, na hatari za wanyama; hatari kutoka kwa wananchi wenzangu na kutoka kwa watu wa mataifa mengine; hatari za mjini, hatari za porini, hatari za baharini, hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. Nimefanya kazi na kutaabika, nimekesha bila usingizi mara nyingi; nimekuwa na njaa na kiu; mara nyingi nimefunga na kukaa katika baridi bila nguo. Na, licha ya mengine mengi, kila siku nakabiliwa na shughuli za makanisa yote. Kama mtu yeyote ni dhaifu, nami pia ni dhaifu; mtu yeyote akikwazwa, nami pia huwa na wasiwasi. Ikinilazimu kujivuna, basi, nitajivunia udhaifu wangu. Mungu na Baba wa Bwana Yesu — jina lake litukuzwe milele — yeye anajua kwamba sisemi uongo. Nilipokuwa Damasko, mkuu wa mkoa, aliyekuwa chini ya mfalme Areta, alikuwa akiulinda mji wa Damasko ili anikamate. Lakini, ndani ya kapu kubwa, niliteremshwa nje kupitia katika nafasi ukutani, nikachopoka mikononi mwake. Nitajivuna basi, ingawa haifai! Lakini sasa nitasema juu ya maono na ufunuo alivyonijalia Bwana. Namjua mtu mmoja Mkristo, ambaye miaka kumi na minne iliyopita alinyakuliwa mpaka katika mbingu ya tatu. (Sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua). Narudia: Najua kwamba mtu huyo alinyakuliwa mpaka peponi. (Lakini sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua). Huko akasikia mambo ya siri ambayo binadamu hastahili kuyatamka. Basi, nitajivunia juu ya mtu wa namna hiyo, na si juu yangu mimi binafsi, isipokuwa tu juu ya udhaifu wangu. Kama ningetaka kujivuna singekuwa mpumbavu hata kidogo, maana ningekuwa nasema ukweli tupu. Lakini sitajivuna; sipendi mtu anifikirie zaidi ya vile anavyoona na kusikia kutoka kwangu. Lakini, kusudi mambo haya makuu niliyofunuliwa yasinifanye nilewe majivuno, nilipewa maumivu mwilini kama mwiba, mjumbe wa Shetani mwenye kunipiga, nisijivune kupita kiasi. Nilimsihi Bwana mara tatu kuhusu jambo hili ili linitoke. Lakini akaniambia: “Neema yangu inatosha kwa ajili yako; maana uwezo wangu hukamilishwa zaidi katika udhaifu.” Basi, ni radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu ili uwezo wake Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo nakubali kwa radhi udhaifu, dharau, taabu, udhalimu na mateso, kwa ajili ya Kristo; maana ninapokuwa dhaifu, ndipo ninapokuwa na nguvu. Nimekuwa kama mpumbavu, lakini nyinyi mmenilazimisha kuwa hivyo. Nyinyi ndio mngalipaswa kunisifu. Maana, ingawa mimi si kitu, kwa vyovyote, mimi si mdogo kuliko hao “mitume wakuu.” Miujiza na maajabu yaoneshayo wazi kwamba mimi ni mtume yalifanyika miongoni mwenu kwa uvumilivu wote. Je, mlipungukiwa nini zaidi kuliko makanisa mengine, isipokuwa tu kwamba mimi kwa upande wangu sikuwasumbueni kupata msaada wenu? Samahani kwa kuwakoseeni haki hiyo! Sasa niko tayari kabisa kuja kwenu mara ya tatu, na sitawasumbua. Maana ninachotafuta si mali zenu, bali ni nyinyi wenyewe. Ni kawaida ya wazazi kuwawekea watoto wao akiba, na si watoto kuwawekea wazazi wao. Mimi ni radhi kabisa kutumia nilicho nacho, na hata kujitolea mimi mwenyewe kabisa, kwa faida ya roho zenu. Je, mtanipenda kidogo ati kwa kuwa mimi nawapenda nyinyi mno? Basi, mtakubali kwamba sikuwa mzigo kwenu. Lakini labda mtu mwingine atasema: “Kwa vile Paulo ni mwerevu, amewafanyieni ulaghai.” Je, mimi niliwanyonyeni kwa njia ya mjumbe yeyote niliyemtuma kwenu? Mimi nilimwita Tito, nikamtuma kwenu na ndugu yetu mwingine. Je, Tito aliwanyonyeni? Je, hamjui kwamba sisi tumekuwa tukiongozwa na roho yuleyule, na mwenendo wetu ni mmoja? Labda mnafikiri kwamba mpaka sasa tumekuwa tukijitetea wenyewe mbele yenu! Lakini, tunasema mambo haya mbele ya Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo. Mambo hayo yote, wapenzi wangu, ni kwa ajili ya kuwajenga nyinyi. Naogopa, huenda nitakapokuja kwenu nitawakuta katika hali nisiyopenda, nami itanilazimu kuwa katika hali msiyoipenda. Naogopa huenda kukawa na ugomvi, wivu, uhasama, ubishi, masengenyo, kunongona, majivuno na fujo kati yenu. Naogopa huenda hapo nitakapokuja safari ijayo Mungu wangu atanifanya niaibike mbele yenu, nami nitaomboleza kwa ajili ya wengi wa wale waliotenda dhambi lakini hawakujuta huo uchafu, tamaa zao mbaya na uzinzi waliokuwa wamefanya. Hii ni mara yangu ya tatu kuja kwenu. “Kila tatizo litatatuliwa kwa ushahidi wa watu wawili au watatu,” yasema Maandiko. Nilikwisha sema, na kama ilivyokuwa safari ya pili, sasa nasema tena nikiwa mbali: Wale wote waliotenda uovu bila kutubu, na pia wale wengine, nitakapokuja, sitakuwa na huruma. Mtajionea wenyewe kwamba Kristo anasema ndani yangu. Kwenu Kristo si dhaifu; bali nguvu yake yafanya kazi miongoni mwenu. Maana hata kama alisulubiwa kwa sababu ya udhaifu, lakini sasa anaishi kwa uwezo wa Mungu. Sisi pia tu dhaifu kwa kuungana naye lakini tutaishi naye kwa uwezo wa Mungu kwa ajili yenu. Jichunguzeni nyinyi wenyewe mpate kujua kama kweli mnayo imani. Jichunguzeni nyinyi wenyewe. Je, hamjui kwamba Kristo Yesu yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi nyinyi mmeshindwa. Lakini natumaini kwamba nyinyi mnajua kuwa sisi hatukushindwa. Tunamwomba Mungu msifanye uovu wowote, lakini si kusudi tuonekane kama watu waliokwisha faulu, bali mpate kutenda mema, hata kama sisi tunaonekana kuwa tumeshindwa. Maana hatuwezi kuupinga ukweli; uwezo tulio nao ni wa kuuendeleza ukweli. Tunafurahi kwamba sisi tu dhaifu, lakini nyinyi mna nguvu; kwa hiyo tunaomba mpate kuwa wakamilifu. Basi, ninaandika barua hii nikiwa mbali, ili nitakapofika kwenu nisilazimike kuwa mkali kwenu kwa kutumia ule uwezo alionipa Bwana; naam, uwezo wa kujenga na si wa kubomoa. Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Salimianeni kwa ishara ya upendo. Watu wote wa Mungu huku wanawasalimuni. Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na umoja wa Roho Mtakatifu, viwe nanyi nyote. Mimi Paulo niliye mtume si kwa mamlaka ya binadamu, wala si kwa nguvu ya mtu, bali kwa uwezo wa Yesu Kristo na wa Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu, na ndugu wote walio pamoja nami tunayasalimu makanisa ya Galatia. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. Kristo alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na mapenzi ya Mungu wetu na Baba, ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu mbaya wa sasa. Kwake yeye uwe utukufu milele na milele! Amina. Nashangaa kwamba muda mfupi tu umepita, nanyi mnamwasi Mungu aliyewaita kwa neema ya Kristo, na mnafuata injili ya namna nyingine. Lakini hakuna injili nyingine. Ukweli ni kwamba wako watu wanaowavurugeni, watu wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo. Lakini, hata kama mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni, atawahubirieni injili tofauti na ile tuliyowahubirieni sisi, basi huyo na alaaniwe! Tulikwisha sema, na sasa nasema tena: Kama mtu yeyote anawahubirieni injili ya aina nyingine, tofauti na ile mliyokwisha pokea, huyo na alaaniwe! Sasa nataka kibali cha nani: Cha binadamu, ama cha Mungu? Au je, nataka kuwapendeza watu? Kama ningefanya hivyo, mimi singekuwa kamwe mtumishi wa Kristo. Ndugu, napenda mfahamu kwamba ile Injili niliyoihubiri si ujumbe wa kibinadamu. Wala mimi sikuipokea kutoka kwa binadamu, wala sikufundishwa na mtu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia. Bila shaka mlikwisha sikia jinsi nilivyokuwa ninaishi zamani kwa kuzingatia dini ya Kiyahudi, na jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kupita kiasi na kutaka kuliharibu kabisa. Naam, mimi niliwashinda wengi wa wananchi wenzangu wa rika langu katika kuizingatia dini ya Kiyahudi, nikajitahidi sana kuyashika mapokeo ya wazee wetu. Lakini Mungu, kwa neema yake, alikuwa ameniteua hata kabla sijazaliwa, akaniita nimtumikie. Mara tu alipoamua kunifunulia Mwanawe kusudi niihubiri Habari Njema yake kwa watu wa mataifa mengine, bila kutafuta maoni ya binadamu, na bila kwenda kwanza Yerusalemu kwa wale waliopata kuwa mitume kabla yangu, nilikwenda kwanza Arabia, kisha nikarudi tena Damasko. Ilikuwa tu baada ya miaka mitatu, ndipo nilipokwenda Yerusalemu kuonana na Kefa; nilikaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. Haya ninayowaandikieni, Mungu anajua; sisemi uongo. Baadaye nilikwenda katika tarafa za Siria na Kilikia. Wakati huo, mimi binafsi sikujulikana kwa jumuiya za Wakristo kule Yudea. Walichokuwa wanajua ni kile tu walichosikia: “Mtu yule aliyekuwa akitutesa hapo awali, sasa anaihubiri imani ileile aliyokuwa anajaribu kuiangamiza.” Basi, wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu. Baada ya miaka kumi na minne, nilikwenda tena Yerusalemu pamoja na Barnaba; nilimchukua pia Tito pamoja nami. Kwenda kwangu kulitokana na ufunuo alionipa Mungu. Katika kikao cha faragha niliwaeleza hao viongozi ujumbe wa Injili niliohubiri kwa watu wa mataifa. Nilifanya hivyo kusudi kazi yangu niliyokuwa nimefanya, na ile ninayofanya sasa, isije ikawa bure. Lakini, hata mwenzangu Tito, ambaye ni Mgiriki, hakulazimika kutahiriwa, ingawa kulikuwa na ndugu wengine wa uongo waliotaka atahiriwe. Watu hawa walijiingiza kwa ujanja na kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika kuungana na Kristo Yesu, ili wapate kutufanya watumwa. Hatukukubaliana nao hata kidogo ili ukweli wa Injili ubaki nanyi daima. Lakini watu hawa wanaosemekana kuwa ni viongozi — kama kweli walikuwa hivyo au sivyo, kwangu si kitu, maana Mungu hahukumu kwa kuangalia mambo ya nje — watu hawa hawakuwa na mawazo ya kuniongezea. Badala yake, walitambua kwamba Mungu alikuwa amenituma kuhubiri Injili kwa watu wa mataifa mengine kama vile Petro alivyokuwa ametumwa kuihubiri kwa Wayahudi. Maana, yule aliyemwezesha Petro kuwa mtume kwa Wayahudi, ndiye aliyeniwezesha nami pia kuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine. Basi, Yakobo, Kefa na Yohane, ambao waonekana kuwa viongozi wakuu, walitambua kwamba Mungu alinijalia neema hiyo, wakatushika sisi mkono, yaani Barnaba na mimi, iwe ishara ya ushirikiano. Sisi ilitupasa tukafanye kazi kati ya watu wa mataifa mengine, na wao kati ya Wayahudi. Wakatuomba lakini kitu kimoja: Tuwakumbuke maskini; jambo ambalo nimekuwa nikijitahidi kutekeleza. Lakini Kefa alipofika Antiokia nilimpinga waziwazi maana alikuwa amekosea. Awali, kabla ya watu kadhaa waliokuwa wametumwa na Yakobo kuwasili hapo, Petro alikuwa akila pamoja na watu wa mataifa mengine. Lakini, baada ya hao watu kufika, aliacha kabisa kula pamoja na watu wa mataifa mengine, kwa kuogopa kikundi cha waliosisitiza tohara. Hata ndugu wengine Wayahudi walimuunga mkono Petro katika kitendo hiki cha unafiki, naye Barnaba akakumbwa na huo unafiki wao. Basi, nilipoona kuwa msimamo wao kuhusu ukweli wa Injili haukuwa umenyooka, nikamwambia Kefa mbele ya watu wote: “Ingawa wewe ni Myahudi, unaishi kama watu wa mataifa mengine na si kama Myahudi! Unawezaje, basi kujaribu kuwalazimisha watu wa mataifa mengine kuishi kama Wayahudi?” Kweli, sisi kwa asili ni Wayahudi, na si watu wa mataifa mengine wenye dhambi! Lakini, tunajua kwa hakika kwamba mtu hawezi kufanywa mwadilifu kwa kuitii sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo. Na sisi pia tumemwamini Yesu Kristo ili tupate kufanywa waadilifu kwa njia ya imani yetu kwa Kristo, na si kwa kuitii sheria. Sasa, ikiwa katika kutafuta tufanywe waadilifu kwa kuungana na Kristo sisi tunaonekana kuwa wenye dhambi, je, jambo hili lina maana kwamba Kristo anasaidia utendaji wa dhambi? Hata kidogo! Lakini ikiwa ninajenga tena kile nilichokwisha bomoa, basi nahakikisha kwamba mimi ni mhalifu. Maana, kuhusu sheria hiyo, mimi nimekufa; sheria yenyewe iliniua, nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. Mimi nimeuawa pamoja na Kristo msalabani, na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa naishi kwa imani, imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu. Sipendi kuikataa neema ya Mungu. Kama mtu hufanywa mwadilifu kwa njia ya sheria, basi, Kristo alikufa bure! Enyi Wagalatia, mmekuwa wajinga kweli! Ni nani aliyewaroga? Habari juu ya kusulubiwa kwake Yesu Kristo ilielezwa waziwazi mbele ya macho yenu. Napenda kujua tu kitu kimoja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa sababu ya kutimiza matakwa ya sheria ama kwa sababu ya kuisikia na kuiamini Injili? Je, nyinyi ni wajinga kiasi hicho? Nyinyi mlianza yote kwa msaada wa Roho, je, mnataka sasa kumaliza kwa nguvu zenu wenyewe? Je, mambo yale yote yaliyowapata nyinyi yamekuwa bure tu? Haiwezekani! Je, Mungu huwajalia Roho na kutenda miujiza kati yenu ati kwa sababu mnatimiza yanayotakiwa na sheria, ama kwa sababu mnasikia Injili na kuiamini? Chukueni kwa mfano habari za Abrahamu: Yeye alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu. Sasa basi, jueni kwamba watu wenye kumwamini ndio walio watoto halisi wa Abrahamu. Maandiko Matakatifu yalionesha kabla kwamba Mungu atawafanya watu wa mataifa kuwa waadilifu kwa njia ya imani. Hivyo Maandiko Matakatifu yalitangulia kumtangazia Abrahamu Habari Njema: “Katika wewe mataifa yote yatabarikiwa.” Basi, wale walio na imani wanabarikiwa pamoja na Abrahamu aliyeamini. Lakini wote wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na sheria, wako chini ya laana. Maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Yeyote asiyeshika na kutimiza yote yaliyoandikwa katika kitabu cha sheria, yuko chini ya laana.” Ni dhahiri kwamba sheria haiwezi kumfanya mtu kuwa mwadilifu; maana Maandiko yasema: “Mwadilifu kwa imani ataishi.” Lakini sheria haitegemei imani, ila Maandiko yasema: “Mwenye kutimiza yanayotakiwa na sheria ataishi.” Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: “Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa.” Jambo hili lilifanyika kusudi ile baraka aliyopewa Abrahamu iwashukie watu wa mataifa mengine kwa njia ya Kristo, na ili kwa imani, tumpokee yule Roho ambaye Mungu alituahidia. Ndugu, nitawapeni mfano kutoka maisha yetu ya kila siku. Fikirini juu ya mkataba kati ya watu wawili. Mkataba ukisha fanyika na kutiwa sahihi hapana mtu anayeuweka kando au kuuongezea kitu. Basi, Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: “Na wazawa wake,” yaani wengi, bali yasema, “Na mzawa wake,” yaani mmoja, naye ndiye Kristo. Ninachotaka kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake, akalithibitisha; sheria ambayo ilitokea miaka 430 baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano wala kuibatilisha hiyo ahadi. Maana, kama zawadi ya Mungu inategemea sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu. Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi. Ya nini basi, sheria? Iliongezwa hapo ili kuonesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. Ama hakika, mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja. Je, sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uhai, basi, tungeweza kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria. Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi aliyotoa Mungu, kwa kumwamini Yesu Kristo. Kabla ya kujaliwa imani, sheria ilitufanya wafungwa, tukingojea imani hiyo ifunuliwe. Basi, hiyo sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani tufanywe waadilifu mbele yake Mungu. Lakini kwa vile ile imani imekwisha fika, sisi hatuko tena chini ya mlezi. Kwa njia ya imani, nyinyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu kwa kuungana na Kristo. Nyinyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja kwa kuungana na Kristo Yesu. Ikiwa nyinyi ni wa Kristo, basi ni wazawa wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu. Basi, nasema hivi: Mrithi, akiwa bado mtoto, hawi tofauti na mtumwa ingawaje mali yote ni yake. Wakati huo wote yuko chini ya walezi na wadhamini mpaka wakati ule uliowekwa na baba yake. Hali kadhalika na sisi tulipokuwa bado watoto, tulikuwa watumwa wa pepo watawala wa ulimwengu. Lakini wakati ule maalumu ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya sheria, apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu. Kwa vile sasa nyinyi ni wanawe, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho ambaye hulia “Aba,” yaani “Baba.” Basi, wewe si mtumwa tena, bali mwana. Na ikiwa ni mwana, basi, wewe utapokea yote Mungu aliyowawekea watoto wake. Zamani hamkumjua Mungu na hivyo mliitumikia miungu isiyo miungu kweli. Lakini sasa, kwa vile mnamjua Mungu, au tuseme mnajulikana na Mungu, mnawezaje tena kurudi kwa wale pepo maskini na dhaifu hata kutaka kuwatumikia tena? Bado mnaadhimisha siku, miezi na miaka! Nahofu kwamba labda kazi niliyoifanya kwa ajili yenu imepotea bure! Ndugu, nawasihi muwe kama mimi, kwa vile hata mimi nimekuwa kama nyinyi. Hamkunitendea ubaya wowote. Mnajua kwamba ugonjwa wangu ndio ulionipatia fursa ya kuwahubirieni Injili kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, wakati ule hamkunidharau wala kunikataa kwa sababu ya udhaifu wangu ingawa mlishawishiwa kufanya hivyo; lakini mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama vile ningekuwa Kristo Yesu mwenyewe. Mlikuwa wenye furaha; sasa kumetokea nini? Naapa kwamba wakati ule mngaliweza hata kuyangoa macho yenu na kunipa mimi. Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa sababu ya kuwaambieni ukweli? Hao watu wengine wanawahangaikia nyinyi, lakini nia yao si njema. Wanataka kuwatenganisha nami ili nyinyi muwahangaikie wao. Kwa kweli ni jambo jema daima kuwahangaikia wengine katika mambo mema, na si tu wakati mimi nipo pamoja nanyi. Watoto wangu, kama vile mama mjamzito anavyotaabika wakati wa kujifungua, mimi nataabika tena kwa ajili yenu mpaka hapo hali yake Kristo itakapoundwa ndani yenu. Laiti ningekuwa pamoja nanyi sasa, maana ningalipata msimamo ufaao juu yenu! Nina wasiwasi sana nanyi! Niambieni, enyi mnaopenda kutawaliwa na sheria: Je, mnasikia isemavyo sheria? Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Abrahamu alikuwa na watoto wawili: Mmoja kwa mwanamke mtumwa, na wa pili kwa mwanamke huru. Yule wa mwanamke mtumwa alizaliwa kama kawaida, lakini yule wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu. Mambo hayo yamekuwa mfano; mama hao wawili ni mfano wa maagano mawili; la kwanza ni lile lililofanyika mlimani Sinai, mwakilishi wake ni Hagari, na watoto wake wanazaliwa utumwani. Hagari anawakilisha mlima Sinai ulioko Arabia, na ni mfano wa Yerusalemu ya sasa, ulio mtumwa pamoja na watoto wake. Lakini Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu. Maana imeandikwa: “Furahi, ewe uliye tasa usiyezaa; paza sauti wewe usiyepata kujifungua mtoto; maana watoto wa yule aliyeachwa ni wengi kuliko wa yule aliye na mume.” Sasa, basi, ndugu zangu, nyinyi ni watoto wa Mungu kutokana na ahadi yake kama alivyokuwa Isaka. Lakini kama vile siku zile yule mtoto aliyezaliwa kwa njia ya kawaida alimdhulumu yule aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho wa Mungu, vivyo hivyo na siku hizi. Lakini Maandiko Matakatifu yasemaje? Yasema: “Mfukuze mama mtumwa pamoja na mwanawe; maana mtoto wa mtumwa hatarithi pamoja na mtoto wa mama huru.” Hivyo basi, ndugu, sisi si watoto wa mtumwa bali wa mama huru. Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Basi, simameni imara wala msikubali tena kuwa chini ya nira ya utumwa. Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote. Nasema tena wazi: Kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika sheria yote. Kama mnatazamia kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu. Kwa upande wetu, lakini, sisi tunangojea kwa matumaini kwa nguvu ya Roho tufanywe waadilifu kwa njia ya imani. Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo. Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi, aliyewazuia kuuzingatia ukweli? Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni. “Chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!” Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba nyinyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni — awe nani au nani — hakika ataadhibiwa. Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote. Laiti hao wanaowavurugeni wangejihasi wenyewe! Nyinyi ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo. Maana sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe! Basi, nasema hivi: Mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka nyinyi wenyewe. Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya sheria. Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: Uzinzi, uasherati, ufisadi; kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano; husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: Watu wanaotenda mambo hayo hawataupata ufalme wa Mungu uwe wao. Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Hakuna sheria inayoweza kupinga mambo hayo. Wale walio na Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake. Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu. Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, nyinyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa. Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo. Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe. Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine. Maana kila mmoja anapaswa kuubeba mzigo wake mwenyewe. Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake. Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna. Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uhai wa milele. Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake. Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu. Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe. Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha nyinyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: Kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo. Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; huwataka nyinyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu. Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya. Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli — watu wa Mungu. Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu. Ndugu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amina. Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, nawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Efeso, mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni. Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake, Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia. Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu ambayo ametujalia katika Mwanae mpenzi! Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake aliyotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote Mungu alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo. Mpango huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo. Katika kuungana na Kristo, sisi tumerithishwa wokovu kama tulivyopangiwa kadiri ya azimio lake Mungu atekelezaye kila kitu kulingana na uamuzi na matakwa yake. Basi, sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu! Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonesha kuwa nyinyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia. Huyu Roho ni dhamana ya kupata yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake! Kwa sababu hiyo, tangu niliposikia juu ya imani yenu kwa Bwana Yesu, na mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu, sijaacha kamwe kumshukuru Mungu kwa ajili yenu. Ninawakumbuka katika sala zangu, ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mtukufu, awajalieni Roho wake atakayewapa hekima na kuwafunulieni Mungu mpate kumjua. Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake, mpate kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo huo unaofanya kazi ndani yetu ni sawa na nguvu ile kuu mno aliyomfufua nayo Kristo kutoka kwa wafu, akamketisha upande wake wa kulia mbinguni. Huko, Kristo anatawala juu ya kila tawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao. Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa akiwa mkuu wa vitu vyote. Kanisa ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila mahali. Nyinyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa na dhambi zenu. Wakati ule mliishi kufuatana na mtindo mbaya wa ulimwengu huu, mkawa mnamtii mtawala wa pepo wenye nguvu wa anga, pepo ambao huwatawala sasa watu wasiomtii Mungu. Na hata sisi sote tulikuwa kama wao; tuliishi kufuatana na tamaa zetu za kidunia na kufanya tu mambo yale yaliyoipendeza miili na akili zetu. Kidunia, sisi kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu. Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika, hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu nyinyi mmeokolewa. Kwa kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni. Ndivyo alivyopenda kuonesha kwa watu wa nyakati za baadaye ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu. Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu. Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu. Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende. Nyinyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine — mnaoitwa, “Wasiotahiriwa” na Wayahudi ambao hujiita, “Waliotahiriwa,” (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao) — kumbukeni mlivyokuwa zamani. Wakati ule nyinyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu katika yale maagano aliyoahidi Mungu. Mlikuwa bila matumaini na kama watu wasiomjua Mungu hapa duniani. Lakini sasa, kwa kuungana na Kristo Yesu, nyinyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo. Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ule ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui. Aliiondoa ile sheria pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani. Kwa mwili wake, Kristo aliuangamiza uadui wao; kwa msalaba wake aliziunganisha jamii hizo kuwa moja na kuzipatanisha na Mungu. Basi, Kristo alikuja akahubiri Habari Njema ya amani kwenu nyinyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu. Hivyo, kwa njia yake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, tunaweza kumwendea Baba kwa Roho mmoja. Basi, nyinyi si wageni tena, wala si watu wa nje. Nyinyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu. Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi. Yeye ndiye mwenye kuliunganisha jengo lote na kulikuza hata liwe hekalu takatifu kwa ajili ya Bwana. Katika kuungana naye, nyinyi pia mnajengwa pamoja na wote wengine, muwe makao ya Mungu kwa njia ya Roho wake. Kutokana na hayo, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu, namwomba Mungu. Bila shaka mmekwisha sikia kwamba Mungu, kwa neema yake, alinikabidhi kazi hii niifanye kwa faida yenu. Mimi nilijulishwa kwa njia ya ufunuo mpango wake uliofichika. (Nimeandika kwa ufupi juu ya jambo hili, nanyi mkiyasoma maneno yangu mtaweza kujua jinsi ninavyoielewa siri hiyo ya Kristo). Zamani watu hawakujulishwa siri hiyo; lakini sasa Mungu amewajulisha mitume na manabii wake watakatifu kwa njia ya Roho. Siri yenyewe ni hii: Kwa njia ya Injili watu wa mataifa mengine wanapata sehemu yao pamoja na Wayahudi katika zile baraka za Mungu; wao ni viungo vya mwili uleule, na wanashiriki ahadi ileile aliyofanya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Mimi nimefanywa kuwa mtumishi wa Injili kwa neema ya pekee aliyonijalia Mungu kwa uwezo wake mkuu. Mimi ni mdogo kuliko watu wote wa Mungu; lakini amenijalia neema yake, ili niwahubirie watu wa mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; tena niwaangazie watu wote waone jinsi mpango wa Mungu uliofichika unavyotekelezwa. Mungu aliye Muumba wa vitu vyote alificha hiyo siri yake tangu milele, kusudi sasa, kwa njia ya kanisa, wakuu na wenye enzi wa mbinguni wapate kuitambua hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi. Mungu alifanya jambo hilo kufuatana na azimio lake la milele ambalo amelifanya kwa njia ya Kristo Yesu Bwana wetu. Basi, kwa kuungana na Kristo na kwa imani kwake, sisi tunathubutu kumwendea Mungu kwa matumaini. Kwa hiyo, nawaombeni msife moyo kwa sababu ya mateso ninayopata kwa ajili yenu, maana hayo ni kwa ajili ya utukufu wenu. Kwa sababu hiyo, nampigia magoti Baba, aliye asili ya jamaa zote duniani na mbinguni. Namwomba Mungu, kadiri ya utajiri wa utukufu wake, awajalieni kwa uwezo wa Roho wake, nguvu ya kuwa imara ndani yenu, naye Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani. Namwomba mpate kuwa na mzizi na msingi katika mapendo kusudi muweze kufahamu pamoja na watu wote wa Mungu jinsi upendo wa Kristo ueneavyo kwa mapana na marefu, kwa kimo na kina. Naam, mpate kujua upendo wa Kristo upitao elimu yote, mjazwe kabisa utimilifu wote wa Mungu. Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria; kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele! Amina. Basi, mimi niliye mfungwa kwa kuwa namtumikia Bwana, nawasihi muishi maisha yanayostahili wito mlioitiwa. Muwe daima wanyenyekevu, wapole na wenye saburi; vumilianeni nyinyi kwa nyinyi kwa mapendo. Fanyeni bidii ya kuhifadhi umoja uletwao na Roho kwa kuzingatia amani iliyo kati yenu. Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile tumaini mliloitiwa na Mungu ni moja. Kuna Bwana mmoja, imani moja na ubatizo mmoja; kuna Mungu mmoja na Baba wa wote, ambaye yuko juu ya wote, afanya kazi katika yote na yuko katika yote. Kila mmoja wetu amepewa neema kadiri ya kipimo alichojaliwa na Kristo. Kama yasemavyo Maandiko: “Alipopaa mbinguni juu kabisa, alichukua mateka; aliwapa watu zawadi.” Basi, inaposemwa: “Alipaa juu,” ina maana gani? Maana yake ni kwamba, kwanza alishuka mpaka chini kabisa duniani. Basi, huyo aliyeshuka hapa duniani ndiye aliyepaa juu ya mbingu zote apate kuujaza ulimwengu. Ndiye aliyewapa watu zawadi: Wengine aliwajalia wawe mitume, wengine manabii, wengine wawe waeneza Injili, wengine wachungaji na waalimu. Alifanya hivyo apate kuwatayarisha watu wote wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma ya Kikristo ili kuujenga mwili wa Kristo, na hivyo sote tuufikie umoja wa imani na kumjua Mwana wa Mungu; tuwe watu waliokomaa na kuufikia utimilifu wake Kristo mwenyewe. Basi, hatutakuwa tena kama watoto, tukitupwa na kupeperushwa huko na huko kwa kila upepo wa mafundisho wanayozua watu wadanganyifu ili wawapotoshe wengine kwa hila. Kama tukiuzingatia ukweli kwa moyo wa mapendo tutakua katika kila jambo kulingana na Kristo ambaye ndiye kichwa; chini ya uongozi wake, viungo vyote vya mwili hushikamana pamoja, na mwili wote hutegemezwa kwa msaada wa viungo vyake. Basi, kila kiungo kikitekeleza kazi yake ipasavyo, mwili wote hukua na kujijenga katika upendo. Basi, kwa jina la Bwana, nawaonyeni: Msiishi tena kama watu wasiomjua Mungu, ambao fikira zao zimekuwa upuuzi mtupu, na akili zao zimo gizani. Wako mbali na uhai wa Mungu kwa sababu ya upumbavu ulio ndani yao na ukaidi wao. Wamepotoka na hawana aibu, wamejitosa katika ufisadi; hufanya kwa pupa kila aina ya mambo ya aibu. Lakini nyinyi hamkujifunza hivyo juu ya Kristo. Ni dhahiri kwamba mlisikia barabara habari zake, na mkiwa wafuasi wake mkafundishwa ukweli ulivyo katika Yesu. Basi, acheni mwenendo wenu wa awali, yaani ule utu wenu wa kale uliokuwa unaangamizwa kwa tamaa zake danganyifu. Jirekebisheni upya rohoni na katika fikira zenu. Vaeni hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa mfano wa Mungu na ambayo hujionesha katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu. Kwa hiyo, acheni uongo. Kila mmoja anapaswa kumwambia mwenzake ukweli, maana kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo. Kama mkikasirika, msikubali hasira yenu iwafanye mtende dhambi, na wala msikae na hasira kutwa nzima. Msimpe Ibilisi nafasi. Aliyekuwa akiiba, asiibe tena, bali na aanze kufanya kazi njema kwa mikono yake, apate kuwa na kitu cha kumsaidia mtu aliye maskini. Maneno mabaya hata yasisikike kamwe miongoni mwenu; kila mara maneno yenu yawe ya kufaa na ambayo hujenga na kuwasaidia wengine, ili yawaneemeshe wasikilizaji wenu. Msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, maana Roho huyo ni alama ya Mungu kwenu kwamba nyinyi ni watu wake, na thibitisho kwamba siku itakuja ambapo Mungu atawakomboeni. Basi, achaneni na uhasama, chuki, hasira, kelele na matusi. Acheni kila uovu! Muwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe nyinyi kwa njia ya Kristo. Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana nyinyi ni watoto wake wapenzi. Upendo uongoze maisha yenu kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama tambiko yenye harufu nzuri na sadaka impendezayo Mungu. Kwa vile nyinyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu. Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa. Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mchoyo, (ambao ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika ufalme wa Kristo na wa Mungu. Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii. Basi, msishirikiane nao. Zamani nyinyi mlikuwa gizani, lakini sasa nyinyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga, maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli. Jaribuni kujua yale yanayompendeza Bwana. Msishiriki katika matendo yasiyofaa ya giza, bali yafichueni. Mambo yanayotendwa kwa siri ni aibu hata kuyataja. Lakini kila kitu kikifichuliwa na mwanga, ukweli wake hudhihirishwa; na kila kilichodhihirishwa huwa mwanga. Ndiyo maana Maandiko yasema: “Amka wewe uliyelala, fufuka kutoka kwa wafu, naye Kristo atakuangaza.” Basi, muwe waangalifu jinsi mnavyoishi. Msiishi kama wapumbavu, bali kama wenye hekima. Tumieni vizuri muda mlio nao maana siku hizi ni mbaya. Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana. Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu. Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na Zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu. Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Kila mmoja amstahi mwenzake kwa sababu ya heshima mliyo nayo kwa Kristo. Wake wawatii waume zao kama kumtii Bwana. Maana mume anayo mamlaka juu ya mkewe, kama vile Kristo alivyo na mamlaka juu ya kanisa; naye Kristo mwenyewe hulikomboa kanisa, mwili wake. Kama vile kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo, wake wawatii waume zao katika mambo yote. Nanyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yake. Alifanya hivyo ili kwa neno lake, aliweke wakfu kwa Mungu, baada ya kulifanya safi kwa kuliosha katika maji, kusudi ajipatie kanisa lililo takatifu na safi kabisa, kanisa lisilo na doa, kasoro au chochote cha namna hiyo. Basi, waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. ( Hakuna mtu yeyote auchukiaye mwili wake; badala ya kuuchukia, huulisha na kuuvika. Ndivyo naye Kristo anavyolitunza kanisa, maana sisi ni viungo vya mwili wake). “Kwa sababu hiyo, mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mkewe, nao wawili watakuwa mwili mmoja.” Kuna ukweli uliofichika katika maneno haya, nami naona kwamba yamhusu Kristo na kanisa lake. Lakini yanawahusu nyinyi pia: Kila mume lazima ampende mkewe kama nafsi yake mwenyewe, naye mke anapaswa kumstahi mumewe. Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni jambo jema. “Waheshimu Baba na mama yako,” hii ndiyo amri ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani, “Upate fanaka na kuishi miaka mingi duniani.” Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo. Enyi watumwa, watiini mabwana zenu hapa duniani kwa hofu na kutetemeka; fanyeni hivyo kwa unyofu wa moyo kana kwamba mnamtumikia Kristo. Fanyeni hivyo si tu wakati wanapowatazama ili mjipendekeze kwao, bali tumikieni kwa moyo kama atakavyo Mungu kwa sababu nyinyi ni watumishi wa Kristo. Muwe radhi kutumikia kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili ya watu. Kumbukeni kwamba kila mtu mwenye kutenda mema, awe mtumwa au mtu huru, atapokea tuzo lake kutoka kwa Bwana. Nanyi mnaotumikiwa, watendeeni vivyo hivyo watumwa wenu, na acheni kutumia vitisho. Kumbukeni kwamba nyinyi pia kama vile wao, mnaye Bwana yuleyule mbinguni, naye hatendi kwa ubaguzi. Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu. Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi. Maana vita vyetu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu, wanaomiliki ulimwengu huu wa giza. Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile itakapofika mweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka mwisho, mtakuwa bado imara. Basi, kaeni tayari. Ukweli na uwe kama mkanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani, na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama viatu miguuni mwenu. Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu. Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu. Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu. Niombeeni nami pia ili niongeapo Mungu anijalie cha kusema, niweze kuwajulisha watu fumbo la Injili kwa uthabiti. Mimi ni balozi kwa ajili ya Injili hiyo ingawa sasa niko kifungoni. Ombeni, basi, ili niweze kuwa hodari katika kuitangaza kama inipasavyo. Tukiko, ndugu yetu mpenzi na mtumishi mwaminifu katika kuungana na Bwana, atawapeni habari zangu zote mpate kujua ninachofanya. Namtuma kwenu awapeni habari zetu mpate kuwa na moyo. Ninawatakieni nyinyi ndugu amani, upendo na imani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho. Mimi Paulo na Timotheo, watumishi wa Yesu Kristo, tunawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Filipi ambao mmeunganishwa na Kristo Yesu, pamoja na viongozi na wasaidizi wa kanisa. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu kila ninapowakumbukeni; na kila ninapowaombeeni nyote, nasali kwa furaha, kwa sababu ya jinsi mlivyonisaidia katika kazi ya Injili tangu siku ile ya kwanza mpaka leo. Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu. Hivyo ndivyo ninavyopaswa kuwafikirieni, kwani nawakumbukeni daima moyoni mwangu. Kwa maana nyinyi nyote mmeshiriki katika fadhili aliyonijalia Mungu ya kutetea na kuithibitisha Injili, sasa niwapo kifungoni na pia pale awali nilipokuwa huru. Mungu anajua kuwa ninasema ukweli ninaposisitiza kwamba, kwa upendo uleule wa Yesu Kristo, natamani sana kuwaoneni. Sala yangu ni hii: Naomba upendo wenu uzidi kuongezeka zaidi na zaidi pamoja na ujuzi wa kweli na busara ya kila namna, ili muweze kuchagua jambo lililo bora. Hapo ndipo mtakuwa safi na bila lawama yoyote ile katika siku ile ya Kristo. Maisha yenu yatajazwa mambo yote yaliyo kweli bora, ambayo Yesu Kristo mwenyewe anaweza kuwajalieni, kwa ajili ya utukufu na sifa ya Mungu. Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mambo yote yaliyonipata yamesaidia sana kuieneza Injili. Kutokana na hayo, walinzi wote wa ikulu pamoja na wengine wote hapa wanafahamu kwamba niko kifungoni kwa sababu mimi namtumikia Kristo. Na huku kuweko kwangu kifungoni kumewafanya ndugu wengi kuwa na imani kwa Bwana, hata wanazidi kuwa hodari katika kuutangaza ujumbe wa Mungu bila hofu. Kweli, baadhi yao wanamhubiri Kristo kwa sababu wana wivu na ni watu wagomvi; lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia nzuri. Hawa wanafanya hivyo kwa upendo, kwani wanajua kwamba Mungu amenipa jukumu hili la kuitetea Injili. Hao wengine wanamtangaza Kristo kwa mashindano na si kwa moyo mnyofu, wakidhani kwamba wataniongezea mateso yangu kifungoni. Haidhuru! Mimi nafurahi ikiwa tu watu wanamhubiri Kristo kwa kila njia, iwe ni kwa nia nzuri au kwa nia mbaya. Tena nitaendelea kufurahi, kwani najua kwamba kwa sala zenu na kwa msaada wa Roho wa Yesu Kristo, nitakombolewa. Hamu yangu kubwa na tumaini langu ni kwamba kwa vyovyote sitashindwa katika kutimiza wajibu wangu, bali nitakuwa na moyo thabiti kila wakati na hasa wakati huu, ili kwa maisha yangu yote, niwapo hai au nikifa, nimpatie Kristo heshima. Kwangu, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida zaidi. Lakini, kama kwa kuishi nitaweza kufanya kazi yenye faida zaidi, basi, sijui nichague lipi! Nakabiliwa na haya mawili yaliyo sawa. Natamani kuyaacha maisha haya nikakae pamoja na Kristo, jambo ambalo ni bora zaidi; lakini ni jambo la maana zaidi kwenu kama nikiendelea kuishi. Nina hakika ya jambo hili, na hivyo najua kwamba nitaendelea kuishi pamoja nanyi nyote, ili nipate kuongeza maendeleo yenu na furaha katika imani. Basi, nitakapokuwa nanyi tena mtakuwa na sababu ya kuona fahari juu yangu katika kuungana na Kristo Yesu. Basi, jambo muhimu ni kwamba mwenendo wenu uambatane na matakwa ya Injili ya Kristo, ili kama nikiweza kuja kwenu au nisipoweza, nipate walau kusikia kwamba mnasimama imara mkiwa na lengo moja, na kwamba mnapigana vita kwa pamoja na mnayo nia moja kwa ajili ya imani ya Injili. Msiwaogope maadui zenu, bali muwe hodari daima, na hiyo itawathibitishia kwamba wao watashindwa, nanyi mtashinda kwani Mungu mwenyewe ndiye anayewapeni ushindi. Maana nyinyi mmepewa fadhili ya kumtumikia Kristo si tu kwa kumwamini bali pia kwa kuteswa kwa ajili yake. Sasa mwaweza kushirikiana nami katika kupigana vita. Vita hivi ni vile mlivyoona nikipigana pale awali na ambavyo bado napigana sasa kama mnavyosikia. Je, maisha yenu katika Kristo yanawapeni nguvu? Je, upendo wake unawafarijini? Je, mnao umoja na Roho Mtakatifu na kuoneana huruma na kusikitikiana nyinyi kwa nyinyi? Basi, ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na fikira moja, upendo mmoja, moyo mmoja na nia moja. Msifanye chochote kwa moyo wa fitina au kwa majivuno ya bure; muwe na unyenyekevu nyinyi kwa nyinyi, na kila mmoja amwone mwenzake kuwa bora kuliko yeye mwenyewe. Pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu bali faida ya mwenzake. Muwe na msimamo uleule aliokuwa nao Kristo Yesu: Yeye, kwa asili alikuwa daima Mungu; lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kungangania kwa nguvu. Bali, kwa hiari yake mwenyewe, aliachilia hayo yote, akajitwalia hali ya mtumishi, akawa sawa na wanadamu, akaonekana kama wanadamu. Alijinyenyekesha na kutii mpaka kufa, hata kufa msalabani. Kwa sababu hiyo Mungu alimkweza juu kabisa, akampa jina lililo kuu kuliko majina yote. Ili kwa heshima ya jina la Yesu, viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu, vipige magoti mbele yake, na kila mtu akiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba. Wapenzi wangu, nilipokuwa nanyi mlinitii daima, na hata sasa niwapo mbali nanyi endeleeni kutii. Fanyeni kazi kwa hofu na tetemeko kwa ajili ya ukombozi wenu, kwani Mungu ndiye afanyaye kazi daima ndani yenu, na kuwapeni uwezo wa kutaka na kutekeleza mambo yanayopatana na mpango wake mwenyewe. Fanyeni kila kitu bila kunungunika na bila ubishi, ili mpate kuwa watu safi, wasio na lawama, kama watoto wanyofu wa Mungu wanaoishi katika ulimwengu mbaya na uliopotoka. Mtangara kati yao kama nyota zinavyoliangaza anga, mkishika imara ujumbe wa uhai. Na hapo ndipo nami nitakapokuwa na sababu ya kujivunia katika siku ile ya Kristo, kwani itaonekana dhahiri kwamba bidii yangu na kazi yangu havikupotea bure. Hata ikiwa nitatolewa mhanga pamoja na imani yenu iliyo tambiko kwa Mungu, basi, nafurahi sana na kuwashirikisha nyinyi nyote furaha hiyo. Hali kadhalika nanyi mnapaswa kufurahi na kunishirikisha mimi furaha yenu. Katika kuungana na Bwana Yesu ninalo tumaini kwamba nitaweza kumtuma Timotheo kwenu hivi karibuni, ili nitiwe moyo kwa kupata habari zenu. Sina mtu mwingine kama yeye ambaye anawashughulikieni kwa moyo. Wengine wanashughulikia tu mambo yao wenyewe badala ya kuyashughulikia mambo ya Yesu Kristo. Nyinyi wenyewe mwafahamu jinsi Timotheo alivyo thabiti; yeye na mimi, kama vile mtoto na baba yake, tumefanya kazi pamoja kwa ajili ya Injili. Kwa hiyo natumaini kumtuma kwenu mara nitakapojua jinsi mambo yatakavyoniendea. Na, ninatumaini katika Bwana kwamba nami pia nitaweza kuja kwenu karibuni. Nimeona sina budi kumtuma kwenu ndugu yetu Epafrodito, ambaye ni mwenzangu kazini na vitani na ambaye ni mjumbe wenu aliyenisaidia katika mahitaji yangu. Anayo hamu kubwa ya kuwaoneni nyinyi nyote, na amesikitika sana kwani nyinyi mmepata habari kwamba alikuwa mgonjwa. Naam, alikuwa mgonjwa hata karibu ya kufa. Lakini Mungu alimwonea huruma, na si yeye peke yake, ila na mimi pia ili nisipate uchungu zaidi. Basi, nataka sana kumtuma kwenu, ili mtakapomwona mpate kufurahi tena, nayo huzuni yangu itoweke. Mpokeeni, basi, kwa furaha yote kama ndugu katika Bwana. Mnapaswa kuwastahi watu walio kama yeye, kwani yeye alikuwa hata karibu ya kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, na kuhatarisha maisha yake ili aweze kunipa mimi msaada ule ambao hamkuweza kuuleta nyinyi wenyewe. Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika kuungana na Bwana. Sichoki kurudia yale niliyokwisha andika pale awali, maana yatawaongezeeni usalama. Jihadharini na hao watendao maovu, hao mbwa, watu wanaosisitiza kujikata mwilini. Watu waliotahiriwa kikweli ni sisi, si wao; kwani sisi twamwabudu Mungu kwa njia ya Roho wake, na kuona fahari katika kuungana na Kristo Yesu. Mambo ya nje tu hatuyathamini. Mimi pia ningeweza kuyathamini hayo mambo ya nje; na kama yupo mtu anayefikiri kwamba anaweza kuyathamini hayo mambo ya nje, mimi ninayo sababu kubwa zaidi ya kufikiri hivyo: Mimi nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa kwangu; mimi ni wa taifa la Israeli, kabila la Benyamini, Mwebrania halisi. Kuhusu kuizingatia sheria mimi nilikuwa Mfarisayo, na nilikuwa na bidii sana hata nikalidhulumu kanisa. Kuhusu uadilifu unaopatikana kwa kuitii sheria, mimi nilikuwa bila hatia yoyote. Lakini hayo yote ambayo ningeweza kuyafikiria kuwa ni faida, nimeyaona kuwa ni hasara, kwa ajili ya Kristo. Naam, wala si hayo tu; ila naona kila kitu kuwa ni hasara tupu, kwa ajili ya jambo bora zaidi, yaani kumjua Kristo Yesu Bwana wangu. Kwa ajili yake nimekubali kutupilia mbali kila kitu; nimeyaona hayo yote kuwa ni takataka, ili nimpate Kristo na kuunganishwa naye kabisa. Mimi sitaki tena uadilifu unaotokana na kuitii sheria. Sasa ninao ule uadilifu unaopatikana katika kumwamini Kristo; uadilifu utokao kwa Mungu na ambao unategemea imani. Ninachotaka tu ni kumjua Kristo na kuiona nguvu ya ufufuo wake, kushiriki mateso yake na kufanana naye katika kifo chake, nikitumaini kwamba nami pia nitafufuliwa kutoka kwa wafu. Sijidai kwamba nimekwisha faulu au nimekwisha kuwa mkamilifu. Naendelea kujitahidi kupata lile tuzo ambalo kwalo Kristo amekwisha nipata mimi. Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele. Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu. Sisi sote tuliokomaa tunapaswa kuwa na msimamo huohuo. Lakini kama baadhi yenu wanafikiri vingine, basi, Mungu atawadhihirishieni jambo hilo. Kwa vyovyote, tusonge mbele katika njia hiyohiyo ambayo tumeifuata mpaka hivi sasa. Ndugu zangu, fuateni mfano wangu. Tumewapeni mfano mwema, na hivyo wasikilizeni wale wanaofuata mfano huo. Nimekwisha waambieni jambo hili mara nyingi, na sasa narudia tena kwa machozi: Watu wengi wanaishi kama maadui wa msalaba wa Kristo. Mwisho wao ni kuangamia, kwani tumbo lao ndilo mungu wao; wanaona fahari juu ya mambo yao ya aibu, hufikiria tu mambo ya kidunia. Lakini sisi ni raia wa mbinguni, na twatazamia kwa hamu kubwa Mwokozi aje kutoka mbinguni, Bwana Yesu Kristo. Yeye ataibadili miili yetu dhaifu na kuifanya ifanane na mwili wake mtukufu, kwa nguvu ile ambayo kwayo anaweza kuviweka vitu vyote chini ya utawala wake. Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, ninaotamani sana kuwaoneni, nyinyi mlio furaha yangu na taji ya ushindi wangu, ndivyo basi mnavyopaswa kukaa imara katika kuungana na Bwana, enyi wapenzi wangu. Euodia na Suntike, nawaombeni na kuwasihi mpatane kama ndugu katika Bwana. Nawe ndugu yangu mwaminifu, nakutaka uwasaidie akina mama hao, kwani wamefanya kazi ya kueneza Injili kwa bidii pamoja nami na Klementi na wafanyakazi wenzangu wengine wote ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uhai. Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: Furahini! Upole wenu ujulikane kwa watu wote. Bwana yu karibu. Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, zingatieni mambo mema na yanayostahili kusifiwa; mambo ya kweli na bora; mambo ya haki, safi, ya kupendeza na ya heshima. Tekelezeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu; mambo mliyosikia nimesema na kuona nimeyatenda. Naye Mungu anayetujalia amani atakuwa pamoja nanyi. Katika kuungana na Bwana nimepata furaha kubwa kwamba mwishoni mlipata tena fursa ya kuonesha kwamba mnanikumbuka. Kusema kweli mmekuwa mkinikumbuka daima ila tu hamkupata nafasi ya kuonesha jambo hilo. Sisemi hivyo sasa kwa sababu nahitaji kitu; maana nimejifunza kuridhika na vitu nilivyo navyo. Najua hali ya kutokuwa na vitu na hali ya kuwa na vingi. Nimejizoeza kuridhika katika kila hali na mahali; niwe nina cha kutosha au nina njaa; iwe nina ziada au nimepungukiwa. Naweza kuikabili kila hali kwani Kristo hunipa nguvu. Hata hivyo, nyinyi mlifanya vema kwa kushirikiana nami katika taabu zangu. Nyinyi Wafilipi mwafahamu wenyewe kwamba mwanzoni mwa kuhubiri Habari Njema, nilipokuwa naondoka Makedonia, nyinyi peke yenu ndio kanisa lililonisaidia; nyinyi peke yenu ndio mlioshirikiana nami katika kupokea na kuwapa wengine mahitaji. Nilipokuwa nahitaji msaada kule Thesalonike mliniletea, tena zaidi ya mara moja. Sio kwamba napenda tu kupokea zawadi; ninachotaka ni faida iongezwe katika hazina yenu. Basi, nimekwisha pokea vitu vyote mlivyonipa, tena ni zaidi kuliko nilivyohitaji. Nina kila kitu kwa vile sasa Epafrodito amekwisha niletea zawadi zenu. Zawadi hizi ni kama tambiko yenye harufu nzuri, sadaka inayokubaliwa na kumpendeza Mungu. Basi, Mungu wangu, kwa utajiri wake mkuu kwa njia ya Kristo, atawapeni mahitaji yenu yote. Utukufu uwe kwa Mungu wetu na Baba yetu, milele na milele. Amina. Nawasalimu watu wote wa Mungu walio wake Kristo Yesu. Ndugu walio pamoja nami hapa wanawasalimuni. Watu wote wa Mungu hapa, na hasa wale walio katika ikulu ya mfalme, wanawasalimuni. Nawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Kolosai, ndugu zetu waaminifu katika kuungana na Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu. Daima tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea. Maana tumesikia juu ya imani yenu kwa Kristo Yesu na juu ya mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu. Imani yenu na mapendo yenu vina msingi katika tumaini mlilowekewa mbinguni. Mlipata kusikia juu ya hilo tumaini mara ya kwanza wakati mlipohubiriwa ule ujumbe wa ukweli wa Habari Njema. Injili inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni kote kama vile ilivyofanya kwenu nyinyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema ya Mungu na kuitambua ilivyo kweli. Mlijifunza juu ya neema ya Mungu kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu, ambaye ni mfanyakazi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu. Yeye alitupa habari za upendo wenu mliojaliwa na Roho. Kwa sababu hiyo tumekuwa tukiwaombeeni daima tangu wakati tulipopata habari zenu. Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa matakwa yake, pamoja na hekima yote na ujuzi wa kiroho. Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu. Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili muweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu. Na kwa furaha mshukuruni Baba, aliyewawezesha nyinyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale aliyowawekea watu wake katika ufalme wa mwanga. Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi. Kwake yeye tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana; ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Maana kwake vitu vyote viliumbwa kila kitu duniani na mbinguni, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana: Wenye enzi, watawala, wakuu na wenye nguvu. Vyote viliumbwa kwake na kwa ajili yake. Yeye alikuwako kabla ya vitu vyote; vyote huendelea kuwako kwa uwezo wake. Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa; yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili. Yeye ndiye mwanzo, mzaliwa wa kwanza aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, ili awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote. Maana Mungu alipenda utimilifu wake wote uwe ndani yake. Kwake vitu vyote vilipatanishwa na Mungu: Na kwa damu yake msalabani akafanya amani na vitu vyote duniani na mbinguni. Hapo kwanza nyinyi pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa maadui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu. Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha naye, kusudi awaweke mbele yake mkiwa watakatifu, safi na bila lawama. Mnapaswa, lakini kuendelea na msingi imara katika imani, wala msikubali kutikiswa kutoka katika tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Injili. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Injili ambayo imekwisha hubiriwa kila mtu duniani. Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa. Nami nimefanywa kuwa mtumishi wa kanisa kufuatana na mpango wake Mungu ambao alinikabidhi kwa faida yenu. Mpango wenyewe ni kuutangaza kwa ukamilifu ujumbe wake, ambao ni siri aliyowaficha binadamu wote tangu milele, lakini sasa amewajulisha watu wake. Mungu ametaka kuwajulisha hao jinsi siri hiyo ilivyo kuu na tukufu ambayo imeenea kwa watu wa mataifa, nayo ndiyo hii: Kristo yuko ndani yenu, na jambo hilo lamaanisha kwamba nyinyi mtaushiriki utukufu wa Mungu. Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote; tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo. Kwa madhumuni hayo mimi nafanya kazi na kujitahidi nikiitumia nguvu kuu ya Kristo ifanyayo kazi ndani yangu. Napenda mjue jinsi ninavyofanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, kwa ajili ya watu wa Laodikea na kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona kwa macho. Nafanya hivi kusudi mioyo yao ifarijiwe na kuvutwa pamoja katika upendo, ili wajazwe uthabiti mwingi uletwao na elimu ya kweli. Hapo wataijua siri ya Mungu ambayo ni Kristo mwenyewe. Ndani yake zimefichika hazina zote za hekima na elimu. Basi, nawaambieni, msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa maneno ya uongo hata kama ni ya kuvutia sana. Maana, ingawa mimi niko mbali nanyi kwa mwili, lakini niko pamoja nanyi kwa roho, na ninafurahi kuona uthabiti kamili mnaosimama nao pamoja katika imani yenu kwa Kristo. Maadamu nyinyi mmemkubali Kristo Yesu aliye Bwana, basi, ishini katika muungano naye. Muwe na mizizi ndani yake, mjijenge juu yake na kuwa imara katika imani kama mlivyofundishwa. Muwe na shukrani tele. Angalieni, basi, mtu asiwapotoshe kwa udanganyifu mtupu wa hekima ya kibinadamu, ambayo chanzo chake ni mafundisho ya mapokeo ya watu na ya pepo watawala, na wala si Kristo mwenyewe! Maana, ndani yake Kristo katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu, nanyi mmepewa uhai kamili katika kuungana naye. Yeye yuko juu ya pepo watawala wote na wakuu wote. Katika kuungana na Kristo nyinyi mlitahiriwa, lakini si kwa tohara ifanywayo na watu, bali inayofanywa na Kristo mwenyewe, na ambayo inahusikana na kukombolewa kutoka katika utu wa dhambi. Maana, mlipobatizwa mlizikwa pamoja na Kristo, na katika ubatizo mlifufuliwa pia pamoja naye kwa kuamini katika nguvu ya Mungu ambaye alimfufua Kristo kutoka kwa wafu. Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu nyinyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa nyinyi uhai pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote; alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani. Huko Kristo aliwapokonya nguvu zao hao pepo watawala na wakuu; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwaburuta kama mateka katika msafara wa ushindi wake. Kwa hiyo, basi, msikubali kupewa masharti na mtu yeyote kuhusu vyakula au vinywaji, siku za sherehe, sikukuu ya mwezi mpya au Sabato. Mambo ya aina hiyo ni kivuli tu cha yale yatakayokuja; ukweli wenyewe ndiye Kristo. Msikubali kuhukumiwa na mtu yeyote anayejitakia kuwa wa maana kwa sababu ya maono ya pekee na ambaye anasisitiza juu ya unyenyekevu wa uongo na ibada kwa malaika. Mtu wa namna hiyo amepumbazika kwa fikira danganyifu za kidunia na amejitenga na Kristo aliye kichwa cha huo mwili. Chini ya uongozi wa Kristo, mwili wote unalishwa na kuunganishwa pamoja kwa viungo na mishipa yake, nao hukua kama atakavyo Mungu. Nyinyi mmekufa pamoja na Kristo na kukombolewa katika nguvu za pepo watawala wa ulimwengu. Kwa nini, basi, kuishi tena kama vile mngekuwa wa ulimwengu huu? Ya nini kuwekewa masharti: “Msishike hiki,” “Msionje kile,” “Msiguse kile!” Mambo hayo yote yanahusika na vitu vyenye kuharibika mara tu vinapotumiwa; hayo ni maagizo na mafundisho ya kibinadamu tu. Kweli, masharti hayo yaonekana kuwa ya hekima kwa namna ya ibada wanayojishurutishia, unyenyekevu, na kuutendea mwili kwa ukali; lakini hayafai chochote kuzuia tamaa za mwili. Basi, ikiwa mmefufuka pamoja na Kristo, panieni mambo ya juu, kule Kristo aliko, ameketi upande wa kulia wa Mungu. Muwe na hamu ya mambo ya huko juu, na siyo mambo ya hapa duniani. Maana nyinyi mmekufa na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Uhai wenu halisi ni Kristo, na wakati atakapotokea ndipo nanyi pia mtakapotokea pamoja naye katika utukufu. Basi, ueni chochote kilicho ndani yenu ambacho ni cha kidunia: Uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya na uchu (ambao ni sawa na kuabudu sanamu). Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya Mungu huwajia wote wanaomwasi. Wakati mmoja nyinyi pia mliishi kufuatana na mambo hayo, mlipotawaliwa nayo. Lakini sasa mnapaswa kuachana na mambo haya yote: Hasira, tamaa na uovu; kufuru au maneno yasiyofaa yasitoke kamwe vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwani nyinyi mmekwisha vua ule utu wa kale pamoja na matendo yake yote, mkavaa utu mpya. Huu unaendelea kurekebishwa na Mungu, Muumba wake, kadiri ya mfano wake, ili mpate kumjua Mungu kwa ukamilifu. Katika hali hii, hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu aliye huru. Kristo ni kila kitu, na yumo katika yote. Nyinyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe nyinyi. Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo, kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili. Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo nyinyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani! Ujumbe wa Kristo na ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani. Na, kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake. Enyi wake, watiini waume zenu, kwani ndivyo apendavyo Bwana. Nanyi waume, wapendeni wake zenu, na msiwe wakali kwao. Enyi watoto, watiini wazazi wenu daima maana hiyo humpendeza Bwana. Nanyi wazazi, msiwachukize watoto wenu, la sivyo watakata tamaa. Enyi watumwa, watiini wakuu wenu wa kidunia katika mambo yote, na si tu wakati wanapowatazama kwa kuwa mnataka kujipendekeza kwao; ila fanyeni hivyo kwa moyo wote, kwa sababu ya kumcha Bwana. Kila mfanyacho, fanyeni kwa moyo wote, kwa sababu ya Bwana na si kwa ajili ya mtu. Kumbukeni kwamba atawapeni tuzo lile alilowawekea watu wake. Mtumikieni Kristo Bwana! Atendaye mabaya atalipwa kufuatana na ubaya wake; Mungu hana ubaguzi. Nanyi wakuu, watendeeni watumwa wenu kwa uadilifu na haki, mkikumbuka kwamba nanyi pia mnaye Bwana mbinguni. Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu, mkimshukuru Mungu. Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni. Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo. Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri wakati mlio nao. Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na yaliyokolezwa kwa chumvi na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja. Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote. Ndiyo maana ninamtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu. Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa. Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami, anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni). Naye Yoshua aitwaye Yusto, anawasalimuni. Miongoni mwa Wayahudi waliokwisha pokea imani, hawa tu peke yao, ndio wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu; nao wamekuwa msaada mkubwa kwangu. Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu, anawasalimuni. Daima anawaombeeni nyinyi kwa bidii ili mpate kusimama imara, mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu. Naweza kushuhudia kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya watu wa Laodikea na Hierapoli. Luka, daktari wetu mpenzi, na Dema, wanawasalimuni. Salamu zetu kwa ndugu wa Laodikea. Msalimuni dada Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waumini inayokutana nyumbani kwake. Mkisha soma barua hii, hakikisheni kwamba inasomwa na Wakristo wa Laodikea; na nyinyi fanyeni mpango mpate kuisoma barua waliyoipata wao. Mwambieni Arkipo aitekeleze vizuri ile huduma aliyokabidhiwa na Bwana. Naandika haya kwa mkono wangu mwenyewe: Salamu kutoka kwangu, mimi Paulo. Kumbukeni kwamba niko kifungoni. Neema ya Mungu iwe nanyi. Mimi Paulo, Silwano na Timotheo, kwa jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambayo ni watu wake Mungu Baba, na wa Bwana Yesu Kristo. Tunawatakieni neema na amani. Tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu nyinyi nyote na kuwakumbukeni daima katika sala zetu. Maana, mbele ya Mungu Baba yetu, twakumbuka jinsi mnavyoonesha imani yenu kwa matendo, jinsi upendo wenu unavyowawezesha kufanya kazi kwa bidii, na jinsi tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo lilivyo thabiti. Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua muwe watu wake, maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi; tuliishi kwa manufaa yenu. Nyinyi mlifuata mfano wetu, mkamwiga Bwana. Ingawa mliteswa sana, mliupokea ujumbe huo kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo nyinyi mmekuwa mfano mzuri kwa waamini wote wa Makedonia na Akaya. Maana, kutokana na bidii yenu ujumbe wa Bwana umesikika si huko Makedonia na Akaya tu, bali imani yenu kwa Mungu imeenea popote. Tena hatuhitaji kusema zaidi. Watu hao wanazungumza juu ya ziara yetu kwenu: Jinsi mlivyotukaribisha, jinsi mlivyoziacha sanamu, mkamgeukia Mungu aliye hai na wa kweli, na sasa mwamngojea Mwanae ashuke kutoka mbinguni, yaani Yesu, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu na ambaye anatuokoa katika ghadhabu ya Mungu inayokuja. Ndugu, nyinyi wenyewe mnafahamu kwamba ziara yetu kwenu haikuwa bure. Mnajua jinsi tulivyodhulumiwa na kutukanwa kule Filipi kabla ya kufika kwenu Thesalonike. Ingawa kulikuwa na upinzani mwingi, Mungu wetu alitujalia uhodari wa kuwahubirieni Habari Njema yake. Jambo tunalosisitiza kwenu si jambo linalotegemea uongo au nia mbaya; wala hatupendi kumdanganya mtu yeyote. Sisi twanena daima kama atakavyo Mungu kwani yeye alituona kwamba tunafaa, akatukabidhi hii Habari Njema. Si nia yetu kuwapendeza watu hata kidogo, bali twataka kumpendeza Mungu ambaye anajua mioyo yetu mpaka ndani. Maana kama mjuavyo, sisi hatukutumia maneno ya kubembeleza wala hatukutumia maneno ya kijanja ya kuficha ubinafsi fulani; Mungu ni shahidi! Hatukutafuta sifa kutoka kwa watu, wala kutoka kwenu, wala kutoka kwa mtu yeyote, ingawa sisi tukiwa mitume wa Kristo, tungeweza kudai mambo fulani kwenu. Lakini sisi tulikuwa wapole kati yenu kama alivyo mama kwa watoto wake. Tuliwapenda nyinyi sana hata tukawa tayari kuwashirikisha si tu Habari Njema ya Mungu, bali pia na maisha yetu. Ndivyo mlivyokuwa wapenzi wetu! Ndugu, nyinyi mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi na kutaabika. Tulipowaleteeni Habari Njema ya Mungu tulifanya kazi mchana na usiku kusudi tusiwe mzigo kwa mtu yeyote miongoni mwenu. Nyinyi mnaweza kushuhudia, na Mungu pia ni shahidi, kwamba mwenendo wetu kati yenu nyinyi mnaoamini ulikuwa mzuri, mwadilifu na bila lawama. Mnajua kwamba sisi tulimtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea watoto wake mwenyewe. Tuliwatia moyo, tuliwafariji na kuwahimiza ili mpate kuishi maisha yampendezayo Mungu ambaye anawaiteni mshiriki ufalme na utukufu wake. Tena tunayo sababu nyingine ya kumshukuru Mungu: Tulipowaleteeni ujumbe wa Mungu, nyinyi mliusikia, mkaupokea, si kama vile ujumbe wa binadamu, bali kama ujumbe wa Mungu, na kweli ndivyo ulivyo. Maana Mungu anafanya kazi ndani yenu nyinyi mnaoamini. Ndugu, nyinyi mmepatwa na mambo yaleyale yaliyoyapata makanisa ya Mungu kule Yudea, mambo yaliyowapata watu walio wake Kristo Yesu. Nyinyi mlidhulumiwa na wananchi wenzenu kama vile wao walivyodhulumiwa na wenzao Wayahudi, ambao walimuua Bwana Yesu na manabii, wakatutesa na sisi pia. Watu hao wanamchukiza Mungu, tena ni maadui za kila mtu! Hata walijaribu kutuzuia kuwahubiria watu wa mataifa mengine ujumbe utakaowaletea wokovu. Ndivyo walivyokamilisha orodha ya dhambi zote walizotenda siku zote. Lakini sasa hasira ya Mungu imewaangukia. Ndugu, kuachana kwetu nanyi kulikuwa kwa muda tu, tena kuachana huko kulikuwa kwa mwili tu na si kwa roho. Kitambo kifupi baadaye, tulishikwa na hamu kubwa ya kuwaoneni tena! Kwa hiyo tuliamua kuwatembeleeni tena. Nami, Paulo, nilijaribu kuja kwenu zaidi ya mara moja, lakini Shetani alituzuia. Je, tutakaposimama mbele ya Bwana Yesu wakati atakapokuja, fahari ya ushindi wetu itakuwa nini? Itakuwa ni nyinyi wenyewe; nyinyi ndio tumaini letu na furaha yetu. Naam, nyinyi ni utukufu wetu na furaha yetu! Mwishowe hatukuweza kuvumilia zaidi. Basi, tuliamua kubaki kule Athene peke yetu, na kumtuma kwenu ndugu yetu Timotheo, ambaye ni mfanyakazi mwenzetu kwa ajili ya Mungu katika kuhubiri Habari Njema ya Kristo. Tulimtuma ili awaimarisheni na kuwafarijini, kusudi imani ya mtu yeyote miongoni mwenu isije ikafifia kwa sababu ya taabu hizo. Nyinyi mnajua kwamba tunapaswa kupata mateso. Maana, tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwaambieni kwamba tutateswa; na kama mjuavyo, ndivyo ilivyotukia. Ndio maana nilimtuma Timotheo kwenu. Sikuweza kungoja zaidi, na hivyo nilimtuma nipate habari za imani yenu. Isije ikawa labda Mshawishi aliwajaribuni na kazi yote tuliyofanya miongoni mwenu ikapotea bure! Sasa Timotheo amekwisha rudi, naye ametupa habari za kufurahisha kuhusu imani na upendo wenu. Ametuarifu kwamba mnatukumbuka daima, na kwamba mna hamu ya kutuona sisi kama nasi tulivyo na hamu ya kuwaoneni. Basi, habari za imani yenu zimetutia moyo katika taabu na mateso yetu yote, kwani sasa tunaishi kweli ikiwa nyinyi mnasimama imara katika kuungana na Bwana. Sasa tunaweza kumshukuru Mungu wetu kwa ajili yenu. Tunamshukuru kwa furaha tuliyo nayo mbele yake kwa sababu yenu. Tunazidi kumwomba Mungu usiku na mchana kwa moyo wetu wote ili atupatie fursa ya kuwaoneni uso kwa uso ili tuweze kurekebisha chochote kilichopungua katika imani yenu. Tunamwomba Mungu, Baba yetu mwenyewe, na Bwana wetu Yesu, atutayarishie njia ya kuja kwenu. Bwana awawezeshe nyinyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda nyinyi. Hivyo ataiimarisha mioyo yenu, nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake. Hatimaye, ndugu zangu, mmejifunza kutoka kwetu namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli mmekuwa mnaishi hivyo. Sasa tunawaombeni na kuwasihi kwa jina la Bwana Yesu mfanye vema zaidi. Maana mnayajua yale maagizo tuliyowapeni kwa mamlaka ya Bwana Yesu. Mungu anataka nyinyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa. Kila mwanamume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima, na si kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu. Basi, mtu yeyote asimkosee au kumpunja mwenzake kuhusu jambo hili. Tulikwisha waambieni hayo na kuwaonya kwamba Bwana atawaadhibu wanaofanya mambo hayo. Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali tuishi katika utakatifu. Kwa hiyo basi, anayedharau mafundisho hayo hamdharau mtu, bali anamdharau Mungu mwenyewe anayewapeni Roho wake Mtakatifu. Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Nyinyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana. Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu, tunawaombeni mfanye hata zaidi. Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali. Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu. Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini. Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana, kwamba sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia. Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana. Basi, farijianeni kwa maneno haya. Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira ya mambo haya yatakapotukia. Maana nyinyi wenyewe mwajua kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku. Watu watakapokuwa wanasema: “Kila kitu ni shwari na salama”, ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo. Lakini nyinyi, ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi. Nyinyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza. Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi. Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku. Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma. Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa. Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana nyinyi kwa nyinyi, kama mnavyofanya sasa. Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo. Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu. Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote. Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote. Furahini daima, salini kila wakati na kuwa na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu. Msimpinge Roho Mtakatifu; msidharau unabii. Pimeni kila kitu: Zingatieni kilicho chema, na kuepuka kila aina ya uovu. Mungu mwenyewe anayetupatia amani awatakase nyinyi kabisa kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu — roho, mioyo na miili yenu — mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye anayewaita nyinyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu. Ndugu, tuombeeni na sisi pia. Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo. Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii. Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mimi Paulo, Silwano na Timotheo, kwa jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambayo ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Ndugu, tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana. Ndio maana sisi tunajivunia nyinyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso mnayopata. Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake, nyinyi mtastahili ufalme wake ambao kwa ajili yake mnateseka. Mungu atafanya jambo la haki: Atawalipa mateso wale wanaowatesa nyinyi na kuwapeni nafuu nyinyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake wenye nguvu na miali ya moto, kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu. Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu, wakati atakapokuja siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake na heshima kutoka kwa wote wanaoamini. Nyinyi pia mtakuwa miongoni mwao, kwani mmeuamini ule ujumbe tuliowaletea. Ndiyo maana tunawaombeeni daima. Tunamwomba Mungu wetu awawezesheni kustahili maisha aliyowaitia muyaishi. Tunamwomba, kwa uwezo wake, atimize nia yenu ya kutenda mema na kukamilisha kazi yenu ya imani. Kwa namna hiyo, jina la Bwana wetu Yesu litapata utukufu kutoka kwenu, nanyi mtapata utukufu kutoka kwake kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo. Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa kwetu pamoja, tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu ya madai kwamba siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu. Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Maana siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule uasi utokee na yule Mwovu aonekane, ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa. Yeye hujikuza yeye mwenyewe juu ya kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu, au wanachokiabudu; hata ataingia na kuketi ndani ya hekalu la Mungu akijidai kuwa Mungu. Je, hamkumbuki kwamba niliwaambieni haya yote wakati nilipokuwa pamoja nanyi? Lakini kuna kitu kinachomzuia sasa, nanyi mwakijua kitu hicho. Basi, huyo Mwovu ataonekana wakati wake ufaao. Hata hivyo, Mwovu huyo aliyefichika anafanya kazi sasa, lakini hataonekana mpaka yule anayemzuia aondolewe. Hapo ndipo Mwovu atakapotokea; lakini Bwana Yesu anapokuja atamuua kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kwa mngao wa kuja kwake. Huyo Mwovu atakuja na nguvu za Shetani na kufanya kila namna ya miujiza na maajabu ya uongo, na kutumia udanganyifu wa kila namna kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea. Hao watapotea kwa sababu hawakuupokea na kuupenda ule ukweli ili waokolewe. Ndiyo maana Mungu amewaweka chini ya nguvu ya upotovu, wauamini uongo. Matokeo yake ni kwamba wote wasioamini ukweli, bali wanafurahia dhambi, watahukumiwa. Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu nyinyi ndugu, nyinyi mnaopendwa na Bwana, kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate kuokolewa kwa nguvu ya Roho, mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika ukweli. Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu, simameni imara na kuzingatia yale mafundisho tuliyowafundisheni kwa mahubiri yetu na barua yetu. Tunamwomba Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu ambaye alitupenda na kwa neema yake akatujalia faraja ya milele na tumaini jema, aifariji mioyo yenu na kuwaimarisheni ili muweze daima kutenda na kusema yaliyo mema. Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu. Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanauamini ujumbe huu. Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu. Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni. Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo. Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa. Nyinyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu; hatukula chakula kwa mtu yeyote bila ya kumlipa. Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu. Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano. Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, “Mtu yeyote asiyependa kufanya kazi, asile chakula.” Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine. Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe. Lakini nyinyi ndugu, msichoke kutenda mema. Huenda kwamba huko kuna mtu ambaye hatautii huu ujumbe tunaowapelekeeni katika barua hii. Ikiwa hivyo, basi, mfichueni mtu huyo na msiwe na uhusiano wowote naye, kusudi aone aibu. Lakini msimtendee mtu huyo kama adui, bali mwonyeni kama ndugu. Bwana mwenyewe ambaye ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote. Kwa mkono wangu mwenyewe naandika hivi: Salamu kutoka kwa Paulo! Hivi ndivyo ninavyotia sahihi kila barua; ndivyo ninavyoandika. Tunawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mimi Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo tumaini letu, nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu. Napenda ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao. Waambie waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani. Shabaha ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na imani ya kweli. Watu wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana. Wanapenda kuwa waalimu wa sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo wanayosisitiza. Twajua kwamba sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo. Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na dini na wa kidunia, watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale; sheria imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wezi wa watu, waongo na wanaoapa uongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho sahihi. Mafundisho hayo hupatikana katika injili ya Mungu mtukufu na mwenye heri ambayo mimi nimekabidhiwa niihubiri. Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie, ingawa pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa ninafanya. Lakini Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika kuungana na Kristo Yesu. Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote, lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aoneshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uhai wa milele. Kwake yeye aliye Mfalme wa milele, asiyekufa, asiyeonekana na aliye Mungu pekee — kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina. Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana vita vizuri, na ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na hivyo wakaiharibu imani yao. Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu. Kwanza kabisa, nawasihi muombe dua, msali na kumshukuru Mungu kwa ajili ya watu wote, kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema. Jambo hili ni jema na lampendeza Mungu Mwokozi wetu, ambaye anataka watu wote waokolewe na wapate kuujua ukweli. Maana yuko Mungu mmoja, na pia yuko mmoja anayewapatanisha watu na Mungu, binadamu Kristo Yesu, ambaye alijitoa mwenyewe kuwakomboa watu wote. Huo ulikuwa uthibitisho, wakati ufaao ulipowadia, kwamba Mungu anataka kuwaokoa watu wote. Kwa sababu hiyo mimi nilitumwa niwe mtume na mwalimu wa watu wa mataifa, niutangaze ujumbe wa imani na ukweli. Nasema ukweli; sisemi uongo! Basi, popote mnapokutana kufanya ibada nataka wanaume wasali, watu waliojitolea kweli na ambao wanaweza kuinua mikono yao wakisali bila hasira wala ubishi. Hali kadhalika, nawataka wanawake wawe wanyofu na wenye busara kuhusu mavazi yao; wavae sawasawa na si kwa urembo wa mitindo ya kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa, bali kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wamchao Mungu. Wanawake wanapaswa kukaa kimya na kuwa wanyenyekevu wakati wa kujifunza. Mimi simruhusu mwanamke amfundishe au amtawale mwanamume; anapaswa kukaa kimya. Maana Adamu aliumbwa kwanza, halafu Hawa. Na wala si Adamu aliyedanganywa; bali mwanamke ndiye aliyedanganywa, akaivunja sheria ya Mungu. Hata hivyo, mwanamke ataokolewa kwa kupata watoto, kama akidumu katika imani, upendo, utakatifu na unyofu. Msemo huu ni wa kweli: Mtu anayetaka kuwa askofu, huyo anatamani kazi nzuri. Basi, askofu anapaswa kuwa mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu; ni lazima awe mkarimu na anayeweza kufundisha; asiwe mlevi au mtu wa matata, bali awe mpole, apendaye amani; asiwe mtu wa kupenda fedha; anapaswa awe mtu awezaye kuongoza vema nyumba yake, na kuwafanya watoto wake wawe watii kwa heshima yote. Maana kama mtu hawezi kuongoza vema nyumba yake, atawezaje kulitunza kanisa la Mungu? Mtu ambaye hajakomaa bado katika imani asifanywe kuwa kiongozi katika kanisa, asije akajaa majivuno na kuhukumiwa kama vile Ibilisi alivyohukumiwa. Anapaswa awe mwenye sifa njema kati ya watu walio nje ya kanisa, ili asije akalaumiwa na kuanguka katika mtego wa Ibilisi. Wasaidizi katika kanisa wanapaswa pia kuwa watu wenye tabia njema na wanyofu; wasiwe wanywaji mno wa divai au wenye tamaa ya fedha; wanapaswa kuzingatia kwa dhamiri njema ukweli wa ndani wa imani. Ni lazima kwanza wathibitishwe, na wakionekana kuwa wanafaa, basi, watoe huduma yao. Wake zao wanapaswa pia kuwa na tabia njema, wasiowasengenya watu, wenye kiasi na waaminifu katika mambo yote. Msaidizi katika kanisa lazima awe na mke moja tu, na awezaye kuongoza vema watoto wake na nyumba yake. Maana wasaidizi wanaofanya kazi yao vizuri hujipatia msimamo mzuri, na wanaweza kusema bila hofu juu ya imani yao katika Kristo Yesu. Ninakuandikia barua hii nikiwa na matumaini ya kuja kwako hivi karibuni. Lakini kama nikicheleweshwa, basi, barua hii itakufahamisha mwenendo tunaopaswa kuwa nao katika nyumba ya Mungu, ambayo ni kanisa la Mungu aliye hai, na ambalo ni nguzo na msingi wa ukweli. Hakuna mashaka yoyote juu ya ukuu wa siri ya dini yetu: Alionekana katika umbo la kibinadamu, alithibitishwa na Roho kuwa ni mwadilifu, akaonekana na malaika. Alihubiriwa kati ya mataifa, aliaminiwa ulimwenguni, akachukuliwa juu katika utukufu. Roho asema waziwazi kwamba siku za baadaye watu wengine wataitupilia mbali imani; watazitii roho danganyifu na kufuata mafundisho ya pepo. Mafundisho ya namna hiyo yanaenezwa na watu waongo wadanganyifu, ambao dhamiri zao ziko kama zimechomwa kwa chuma cha moto. Watu hao hufundisha kwamba ni makosa kuoa na pia kula vyakula fulani. Lakini Mungu aliviumba vyakula hivyo, ili wale walio waumini na ambao wanapata kuujua ukweli, wavitumie kwa shukrani. Kila kitu alichoumba Mungu ni chema, wala hakuna kinachohitaji kukataliwa, bali vyote vipokelewe kwa sala ya shukrani, kwa sababu neno la Mungu na sala hukifanya kitu hicho kikubalike kwa Mungu. Kama ukiwapa ndugu wote maagizo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, ukijiendeleza kiroho kwa maneno ya imani na mafundisho ya kweli ambayo wewe umeyafuata. Lakini achana na hadithi zile zisizo za kidini na ambazo hazina maana. Jizoeshe kuishi maisha ya uchaji wa Mungu. Mazoezi ya mwili yana faida yake, lakini mazoezi ya kiroho yana faida za kila namna, maana yanatuahidia uhai katika maisha ya sasa, na pia hayo yanayokuja. Usemi huo ni wa kusadikika kabisa na unastahili kukubaliwa. Sisi tunajitahidi na kufanya kazi kwa bidii kwani tumemwekea tumaini letu Mungu aliye hai ambaye ni Mwokozi wa watu wote, na hasa wale wanaoamini. Wape maagizo hayo na mafundisho hayo. Usikubali mtu yeyote akudharau kwa sababu wewe ni kijana, lakini jitahidi uwe mfano kwa wanaoamini: Katika usemi wako, mwenendo wako, upendo, imani na maisha safi. Tumia wakati wako na juhudi yako katika kusoma hadharani Maandiko Matakatifu, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. Usiache kukitumia kile kipaji cha Kristo ndani yako ulichopewa kwa maneno ya manabii na kwa kuwekewa mikono na wazee. Fikiri kwa makini juu ya hayo yote na kuyatekeleza kusudi maendeleo yako yaonekane na wote. Angalia sana mambo yako mwenyewe na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo, maana ukifanya hivyo, utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza. Usimkemee mwanamume mzee, bali msihi kama vile angekuwa baba yako. Watendee vijana wa kiume kama ndugu zako, wanawake wazee kama mama zako, na vijana wa kike kama dada zako, kwa usafi wote. Waheshimu wanawake wajane walio wajane kweli. Lakini mjane aliye na watoto au wajukuu, hao wanapaswa kujifunza kutimiza wajibu wao wa kidini kwa jamaa zao wenyewe na hivyo kuwalipa wazazi wao na wazee wao, kwani hilo ni jambo la kupendeza mbele ya Mungu. Mwanamke mjane kweli, asiye na mtu wa kumsaidia, amemwekea Mungu tumaini lake na huendelea kusali na kumwomba msaada usiku na mchana. Lakini mwanamke ambaye huishi maisha ya anasa, huyo amekufa, ingawa yu hai. Wape maagizo haya, wasije wakawa na lawama. Lakini kama mtu hawatunzi watu wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani kwake, basi, mtu huyo ameikana imani, na ni mbaya zaidi kuliko mtu asiyeamini. Usimtie katika orodha ya wajane mjane yeyote ambaye hajatimiza miaka sitini. Tena awe amepata kuolewa mara moja tu, na awe mwenye sifa nzuri: Aliyewalea watoto wake vizuri, aliyewakaribisha wageni nyumbani kwake, aliyewaosha miguu watu wa Mungu, aliyewasaidia watu wenye taabu, na aliyejitolea kufanya mambo mema. Usiwaandikishe wajane vijana, kwani kama tamaa zao za maumbile zikizidi kuwa na nguvu zaidi kuliko kujitolea kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena, na wataonekana kukosa uaminifu kuhusu ahadi yao ya pale awali. Wajane kama hao huanza kupoteza wakati wao wakizurura nyumba hata nyumba; tena ubaya zaidi ni kwamba huanza kuwasengenya watu, na kujitia katika mambo ya watu wengine, huku wakisema mambo ambayo hawangepaswa kusema. Kwa hiyo ningependelea wajane vijana waolewe, wapate watoto na kutunza nyumba zao ili maadui zetu wasipewe nafasi ya kusema mambo maovu juu yetu. Kwa maana wajane wengine wamekwisha potoka na kumfuata Shetani. Lakini kama mama Mkristo anao wajane katika jamaa yake, yeye anapaswa kuwatunza na si kuliachia kanisa mzigo huo, ili kanisa liweze kuwatunza wajane wale waliobaki peke yao kabisa. Viongozi wa kanisa wanaowaongoza watu vizuri wanastahili kupata riziki maradufu, hasa wale wanaofanya bidii katika kuhubiri na kufundisha. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Usimfunge ng'ombe kinywa anapopura nafaka,” na tena “Mfanyakazi astahili malipo yake.” Usikubali kupokea mashtaka dhidi ya mzee yasipowakilishwa na mashahidi wawili au watatu. Wale wanaotenda dhambi waonye hadharani, ili wengine wapate kuogopa. Nakuamuru mbele ya Mungu, mbele ya Kristo Yesu na mbele ya malaika watakatifu, uyazingatie maagizo haya bila kuacha hata moja, wala kumpendelea mtu yeyote katika kila unachotenda. Usiharakishe kumwekea mtu yeyote mikono kwa ajili ya kumtumikia Bwana. Usishiriki dhambi za wengine; jiweke katika hali safi. Usinywe maji tu, bali unywe divai kidogo kwa ajili ya tumbo lako, kwani unaugua mara kwa mara. Dhambi za watu wengine huonekana waziwazi, nazo zawatangulia kwenye hukumu; lakini dhambi za wengine huonekana tu baadaye. Vivyo hivyo, matendo mema huonekana waziwazi, na hata yale ambayo si dhahiri hayawezi kufichika. Watumwa wote wanapaswa kuwaheshimu wakuu wao ili kusiwe na sababu ya watu kulitukana jina la Mungu na mafundisho yetu. Watumwa ambao wakuu wao ni Wakristo wasiwadharau kwani ni ndugu zao. Badala yake, wanapaswa kuwatumikia hata vizuri zaidi, maana hao wanaopata faida kutokana na kazi yao ni waumini ambao wanawapenda. Unapaswa kufundisha na kuhubiri mambo haya. Mtu yeyote anayefundisha kinyume cha mambo haya, na ambaye hakubaliani na maneno ya kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo na mafundisho ya uchaji wa Mungu, huyo amejaa majivuno na wala hajui chochote. Ni mtu wa kupenda ubishi na magombano juu ya maneno matupu, na hiyo husababisha wivu, ugomvi, matusi, shuku mbaya, na ubishi usio na kikomo kutoka kwa watu ambao akili zao zimeharibika, na ambao hawana tena ukweli. Wanadhani dini ni njia ya kujipatia utajiri. Kweli kumcha Mungu humfanya mtu awe tajiri sana, ikiwa anatosheka na vitu alivyo navyo. Maana hatukuleta kitu chochote hapa duniani, wala hatutachukua chochote. Kwa hiyo basi, kama tunacho chakula na mavazi, tunapaswa kuridhika navyo. Lakini wale wanaotaka kutajirika huanguka katika majaribu, na kunaswa katika mtego wa tamaa nyingi mbaya za kipumbavu, ambazo huwavuta mpaka kwenye uharibifu na maangamizi. Kwa maana kupenda sana fedha ni chanzo cha uovu wote. Watu wengine wametamani sana kupata fedha hata wakatangatanga mbali na imani, na wameivunja mioyo yao kwa huzuni nyingi. Lakini wewe, mtu wa Mungu, jiepushe na mambo hayo. Zingatia uadilifu, uchaji wa Mungu, imani, upendo, subira na unyenyekevu. Piga mbio kadiri uwezavyo katika shindano la mbio za imani, ukajipatie tuzo la uhai wa milele uliloitiwa wakati ulipokiri imani yako mbele ya mashahidi wengi. Mbele ya Mungu anayevipa vitu vyote uhai, na mbele ya Yesu Kristo aliyetoa ushahidi na kukiri ukweli mbele ya Pontio Pilato, nakuamuru ushike maagizo yako na kuyatii kwa uaminifu mpaka siku ile atakapotokea Bwana wetu Yesu Kristo. Kutokea kwake kutafanyika wakati ufaao uliopangwa na Mungu mwenye heri na aliye Mtawala pekee, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana. Yeye peke yake anaishi milele katika mwanga usioweza kukaribiwa na mtu. Hakuna mtu aliyepata kumwona au awezaye kumwona. Kwake iwe heshima na uwezo wa milele! Amina. Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie. Waamuru watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, na wawe wakarimu na walio tayari kuwashirikisha wengine mali zao. Kwa namna hiyo watajiwekea hazina ambayo itakuwa kwao msingi imara kwa wakati ujao. Hapo wataweza kujipatia uhai ambao ni uhai wa kweli. Timotheo, tunza salama yote yale uliyokabidhiwa. Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ubishi wa kipumbavu juu ya kile wanachokiita watu wengine “Elimu.” Maana wengine wamejidai kuwa na hiyo elimu, na matokeo yake wamepoteza imani. Nawatakieni nyote neema! Mimi Paulo, ambaye Mungu alitaka niwe mtume wa Kristo Yesu ili niutangaze ule uhai tulioahidiwa katika kuungana na Kristo Yesu, nakuandikia wewe mwanangu mpenzi Timotheo. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu. Ninamshukuru Mungu ambaye ninamtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya wazee wangu; namshukuru kila ninapokukumbuka katika sala zangu usiku na mchana. Nakumbuka machozi yako na ninatamani sana kukuona, ili nijazwe furaha. Naikumbuka imani yako ya kweli, imani aliyokuwa nayo nyanya yako Loisi, na pia mama yako Eunike. Nina hakika kwamba wewe pia unayo. Ndio maana nakukumbusha ukiweke motomoto kile kipaji ulichopewa na Mungu wakati nilipokuwekea mikono yangu. Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu. Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unayopewa na Mungu. Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya mastahili ya matendo yetu, bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo kwa ajili ya Kristo Yesu kabla ya wakati, lakini imefunuliwa kwetu sasa kwa kuja kwake Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uhai usio na kifo. Mimi nimechaguliwa niwe mtume na mwalimu kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema, nami nateseka kwa mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba yeye atakilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka siku ile. Shika kwa makini mafundisho yale ya kweli niliyokufundisha na kubaki katika hiyo imani na huo upendo wetu katika kuungana na Kristo Yesu. Jambo lile bora ulilokabidhiwa lilinde kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeishi ndani yetu. Kama unavyojua, watu wote mkoani Asia wameniacha, miongoni mwao wakiwa Fugelo na Hermogene. Bwana aihurumie jamaa ya Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha rohoni mara nyingi, wala hakuona haya kwa kuwa nilikuwa kifungoni, ila mara tu alipofika Roma, alianza kunitafuta kwa bidii mpaka akanipata. Bwana amjalie kupata huruma ya Mungu katika siku ile! Nawe wajua vizuri mengi aliyonifanyia huko Efeso. Basi, wewe mwanangu, uwe na nguvu katika neema tunayopata katika kuungana na Kristo Yesu. Chukua yale mafundisho uliyonisikia nikitangaza mbele ya mashahidi wengi, uyakabidhi kwa watu wanaoaminika, ambao wataweza kuwafundisha wengine pia. Shiriki katika mateso kama askari mwaminifu wa Kristo Yesu. Mwanajeshi vitani hujiepusha na shughuli za maisha ya kawaida, ili aweze kumpendeza mkuu wa jeshi. Mwanariadha yeyote hawezi kushinda na kupata zawadi ya ushindi kama asipozitii sheria za michezo. Mkulima ambaye amefanya kazi ngumu anastahili kupata sehemu ya kwanza ya mavuno. Fikiria hayo ninayosema, kwani Bwana atakuwezesha uelewe kila kitu. Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, aliyekuwa wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Habari Njema ninayoihubiri, na ambayo kwa sababu yake mimi nateseka na nimefungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu haliwezi kufungwa minyororo. Kwa hiyo navumilia kila kitu kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili wao pia wapate ukombozi upatikanao kwa njia ya Yesu Kristo, na ambao huleta utukufu wa milele. Usemi huu ni wa kweli: “Ikiwa tulikufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye. Tukiendelea kuvumilia, tutatawala pia pamoja naye. Tukimkana, naye pia atatukana. Tukikosa kuwa waaminifu, yeye hubaki mwaminifu daima, maana yeye hawezi kujikana mwenyewe.” Basi, wakumbushe watu wako mambo haya na kuwaonya mbele ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia. Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli. Jiepushe na majadiliano yasiyofaa na ya kipumbavu; kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu. Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili. Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto. Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika. Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na juu yake yameandikwa maneno haya: “Bwana anawafahamu wale walio wake,” na “Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na uovu.” Katika nyumba kubwa kuna mabakuli na vyombo vya kila namna: Vingine ni vya fedha na dhahabu, vingine vya mbao na udongo, vingine vya matumizi ya heshima na vingine kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Basi, kama mtu atajitakasa kwa kujitenga mbali na mambo hayo yote maovu, atakuwa chombo cha matumizi ya pekee, kwa sababu amewekwa wakfu, anamfaa Bwana wake na yupo tayari kwa kila kazi njema. Jiepushe na tamaa za ujana, fuata uadilifu, imani, upendo, amani, pamoja na watu wote ambao wanamwomba Bwana kwa moyo safi. Epuka ubishi wa kijinga na kipumbavu; wajua kwamba hayo huleta magomvi. Mtumishi wa Bwana asigombane. Anapaswa kuwa mpole kwa watu wote, mwalimu mwema na mvumilivu, ambaye ni mpole anapowaonya wapinzani wake, kwani huenda Mungu akawajalia nafasi ya kutubu, wakapata kuujua ukweli. Hapo fahamu zao zitawarudia tena, wakaponyoka katika mtego wa Ibilisi aliyewanasa na kuwafanya wayatii matakwa yake. Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu. Watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu; watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema; watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu. Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo. Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina; wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli. Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose. Hao ni watu wa akili potovu na imani ya uongo. Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre. Wewe, lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu, udhalimu na mateso. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote. Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe. Watu waovu na wadanganyifu wataendelea kuwa wabaya, wakidanganya wengine, na wao wenyewe wakidanganywa. Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa ukaukubali kabisa. Wawajua wale waliokuwa waalimu wako, wakumbuka kwamba tangu utoto wako umejua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu. Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili, ili mtu wa Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila kazi njema. Nakuamuru mbele ya Mungu, na mbele ya Kristo Yesu atakayewahukumu watu walio hai na wafu, na kwa sababu anakuja kutawala akiwa Mfalme: Hubiri huo ujumbe, sisitiza kuutangaza (iwe ni wakati wa kufaa au wakati usiofaa), karipia, onya na himiza watu ukiwafundisha kwa uvumilivu wote. Utakuja wakati ambapo watu hawatasikiliza mafundisho ya kweli, ila watafuata tamaa zao wenyewe na kujikusanyia waalimu tele watakaowaambia mambo yale tu ambayo masikio yao yako tayari kusikia. Watakataa kuusikia ukweli, watageukia hadithi za uongo. Wewe, lakini, uwe macho katika kila hali; vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Habari Njema, timiza kikamilifu utumishi wako. Kwa upande wangu mimi, niko karibu kabisa kutolewa tambiko na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimefanya bidii katika mashindano, nimemaliza safari yote na imani nimeitunza. Na sasa imebakia tu kupewa tuzo la ushindi kwa maisha ya uadilifu, tuzo ambalo Bwana, Hakimu wa haki, atanipa mimi siku ile, na wala si mimi tu, ila na wale wote wanaotazamia kwa upendo kutokea kwake. Fanya bidii kuja kwangu karibuni. Dema ameupenda ulimwengu huu akaniacha na kwenda zake Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia, na Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake ndiye aliye hapa pamoja nami. Mpate Marko uje naye, kwa maana ataweza kunisaidia katika kazi yangu. Nilimtuma Tukiko kule Efeso. Utakapokuja niletee koti langu nililoacha kwa Karpo kule Troa; niletee pia vile vitabu, na hasa vile vya ngozi. Yule sonara aitwaye Aleksanda amenitendea maovu mengi; Bwana atamlipa kufuatana na hayo matendo yake. Jihadhari naye kwa sababu aliupinga ujumbe wetu kwa ukali. Wakati nilipojitetea kwa mara ya kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu; wote waliniacha. Mungu asiwahesabie kosa hilo! Lakini Bwana alikaa pamoja nami, akanipa nguvu, hata nikaweza kuutangaza ujumbe wote, watu wa mataifa wausikie; tena nikaokolewa katika hukumu ya kifo kama kinywani mwa simba. Bwana ataniokoa na mambo yote maovu, na kunichukua salama mpaka katika ufalme wake wa mbinguni. Kwake uwe utukufu milele na milele! Amina. Wasalimu Priska na Akula, pamoja na jamaa ya Onesiforo. Erasto alibaki Korintho, naye Trofimo nilimwacha Mileto kwa sababu alikuwa mgonjwa. Fanya bidii kuja kabla ya majira ya baridi. Ebulo, Pudensi, Lino na Klaudio wanakusalimu; vilevile ndugu wengine wote. Bwana awe nawe rohoni mwako. Nawatakieni nyote neema. Mimi Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo naandika. Mimi nimechaguliwa kuijenga imani ya wateule wa Mungu na kuwaongoza waufahamu ukweli wa dini yetu ambayo msingi wake ni tumaini la kupata uhai wa milele. Mungu ambaye hasemi uongo, alituahidia uhai huo kabla ya mwanzo wa nyakati, na wakati ufaao ulipowadia, akaudhihirisha katika ujumbe wake. Mimi nilikabidhiwa ujumbe huo niutangaze kufuatana na amri ya Mungu, Mwokozi wetu. Ninakuandikia wewe Tito, mwanangu wa kweli katika imani tunayoshiriki. Nakutakia neema na amani kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wetu. Nilikuacha Krete ili urekebishe yale mambo ambayo hayakuwa yamekamilika bado, na kuwateua wazee wa kanisa katika kila mji. Kumbuka maagizo yangu: Mzee wa kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini, wasiojulikana kuwa wakorofi au wakaidi. Maana kwa vile kiongozi wa kanisa ni mkurugenzi wa kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiye na hatia. Asiwe mwenye majivuno, mwepesi wa hasira, mlevi, mkorofi au mchoyo. Anapaswa kuwa mkarimu na anayependa mambo mema. Anapaswa kuwa mtu mtaratibu, mwadilifu, mtakatifu na mwenye nidhamu. Ni lazima ashike kikamilifu ujumbe ule wa kuaminika kama unavyofundishwa. Ndivyo atakavyoweza kuwatia wengine moyo kwa mafundisho sahihi na kuyafichua makosa ya wale wanaoyapinga mafundisho hayo. Maana, wako watu wengi, hasa wale walioongoka kutoka dini ya Kiyahudi, ambao ni wakaidi, na wanawapotosha wengine kwa upumbavu wao. Lazima kukomesha maneno yao, kwani wanavuruga jumuiya nzima kwa kufundisha mambo ambayo hawapaswi kufundisha; wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kupata faida ya fedha. Hata mmoja wa manabii wao, ambaye naye pia ni Mkrete, alisema: “Wakrete husema uongo daima; ni kama wanyama wabaya, walafi na wavivu!” Naye alitoboa ukweli; na kwa sababu hiyo, unapaswa kuwakaripia vikali, ili wawe na imani kamilifu. Wasiendelee kushikilia hadithi tupu za Kiyahudi na maagizo ya kibinadamu yanayozuka kwa watu walioukataa ukweli. Kila kitu ni safi kwa watu walio safi; lakini hakuna chochote kilicho safi kwa wale waliochafuliwa na wasioamini, maana dhamiri na akili zao zimechafuliwa. Watu kama hao hujidai kwamba wanamjua Mungu, lakini kwa matendo yao humkana. Ni watu wa kuchukiza mno na wakaidi, hawafai kwa jambo lolote jema. Lakini wewe unapaswa kuhubiri mafundisho sahihi. Waambie wanaume wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu. Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema, ili wawazoezeshe kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto, wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa. Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi. Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako. Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili maadui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu. Watumwa wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao, au kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonesha kwamba wao ni wema na waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu ya Mungu, Mwokozi wetu. Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa, tukiwa tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema. Basi, sema mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau. Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema. Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikilizano, wawe daima wapole kwa kila mtu. Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukachukiana. Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu, ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uhai wa milele tunaotumainia. Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, yaani mambo mazuri na ya kuwafaa watu. Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu. Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye. Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea. Baada ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi. Jitahidi kumsaidia mwanasheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao, na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji. Ni lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa. Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema ya Mungu. Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu, na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkipo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Kila wakati ninaposali, nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu, maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu. Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo. Ndugu, upendo wako umeniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu. Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika kuungana na Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya. Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake. Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni. Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia. Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe. Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Injili. Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika. Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima. Na sasa yeye si mtumwa wa kawaida, ila ni bora zaidi ya mtumwa: Yeye ni ndugu yetu mpenzi. Ni wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi, kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana. Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe. Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi. Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: Mimi Paulo nitalipa! (Tena sina haja ya kusema kwamba wewe unalo deni kwangu la nafsi yako). Naam, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo. Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba. Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni. Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu. Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu. Nawatakieni nyinyi nyote neema ya Bwana Yesu Kristo. Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii, lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu, akamteua avimiliki vitu vyote. Yeye ni mngao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwatakasa binadamu dhambi zao, ameketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu. Mwana ni mkuu kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu kuliko jina lao. Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: “Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa Baba yako.” Wala hakusema juu ya malaika yeyote: “Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu.” Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae, mzaliwa wa kwanza, ulimwenguni alisema: “Malaika wote wa Mungu na wamwabudu.” Lakini kuhusu malaika, alisema: “Amewafanya malaika wake kuwa upepo, na wahudumu wake ndimi za moto.” Lakini kuhusu Mwana, Mungu alisema: “Kiti chako cha enzi, ee Mungu, chadumu milele na milele! Wewe wawatawala watu wako kwa haki. Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Ndiyo maana Mungu, Mungu wako, amekuweka wakfu na kukumiminia furaha kubwa kuliko wenzako.” Na tena: “Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo, mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima, zote zitachakaa kama vazi. Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilishwa kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayatakoma.” Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: “Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.” Malaika ni nini ila roho wanaomtumikia Mungu na ambao hutumwa kuwasaidia wale watakaopokea wokovu? Kwa hiyo tunapaswa kuzingatia kwa makini yote tuliyosikia, tusije tukayakosa. Ujumbe ule waliopewa wazee wetu na malaika ulioneshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili. Basi, sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu, na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli. Mungu pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu, na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake. Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake. Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko: “Mtu ni nini, hata umfikirie; mwanadamu ni nini hata umjali? Ulimfanya tu kidogo kuwa chini ya malaika; umemvika taji ya utukufu na heshima, ukaweka kila kitu chini ya miguu yake.” Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote, yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa. Lakini twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini kuliko malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote. Sasa tunamwona ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka. Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu. Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao, ndugu zake; kama asemavyo: “Ee Mungu, nitawasimulia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao.” Tena asema: “Nitamwekea Mungu tumaini langu.” Na tena: “Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu.” Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili, kwa njia ya kifo chake, amwangamize Ibilisi ambaye ana mamlaka juu ya kifo, na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya kifo. Maana ni wazi kwamba yeye hakuja kuwasaidia malaika, bali kama yasemavyo Maandiko: “Anawasaidia wazawa wa Abrahamu.” Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake kwa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe. Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa. Ndugu zangu, watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu Mtume na Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama. Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu. Lakini Yesu anastahili heshima kubwa kuliko Mose maana mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. Kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote. Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye. Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi wenyewe ni nyumba yake kama tukiendelea kuwa hodari na thabiti katika kile tunachotumainia. Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: “Kama mkisikia sauti yake leo, msiwe wakaidi kama wakati ule waliponiasi kama wakati ule wa majaribio kule jangwani. Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, ingawa walishuhudia matendo yangu kwa miaka arubaini! Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, ‘Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu’. Basi, nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko.’ Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai. Maadamu hiyo “Leo” inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi. Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni. Maandiko yasema hivi: “Kama mkisikia sauti yake leo, msiwe wakaidi kama wakati ule waliponiasi.” Ni akina nani waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri. Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arubaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani. Mungu alipoapa: “Hawataingia mahali pangu pa pumziko,” alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi. Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini. Basi, kwa vile ahadi ya kuingia mahali pa pumziko bado ipo, na tuogope ili yeyote kati yenu asije akashindwa kupata pumziko hilo. Maana Habari Njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale. Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani. Basi, sisi tunaoamini tunapata pumziko hilo aliloahidi Mungu. Kama alivyosema: “Nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko.’” Mungu alisema hayo ingawa kazi yake ilikuwa imekwisha malizika tangu alipoumba ulimwengu. Maana Maandiko yasema mahali fulani kuhusu siku ya saba: “Mungu alipumzika siku ya saba, akaacha kazi zake zote.” Tena jambo hili lasemwa pia: “Hawataingia mahali pangu pa pumziko.” Basi, hiyo ahadi ya kuingia bado ipo, maana wale waliohubiriwa Habari Njema pale awali walishindwa kuingia humo kwa sababu walikosa kutii. Mungu aliweka siku nyingine ambayo inaitwa “Leo,” akasema baadaye kwa njia ya Daudi maneno yaliyokwisha tajwa: “Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiwe wakaidi.” Kama Yoshua angekuwa amewapa watu hao hilo pumziko, Mungu hangalisema baadaye juu ya siku nyingine. Kwa hiyo, basi, bado kuna kupumzika kwa watu wa Mungu. Maana, kila aingiaye mahali pa pumziko la Mungu atapumzika kutoka katika kazi yake kama vile pia Mungu alivyopumzika kutoka kazi yake. Basi, tujitahidi kuingia katika pumziko hilo, ili asiwepo yeyote miongoni mwetu atakayekataa kutii kama walivyofanya wao. Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali kuliko upanga wenye makali kuwili. Hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho hukutana, mpaka pale vikutanapo viungo vya mwili na uboho. Neno hilo huchambua nia na fikira za mioyo ya watu. Hakuna kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi mbele ya macho yake yeye ambaye kwake tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu. Basi, tuzingatie kwa makini imani tunayoiungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka mbinguni; Yesu, Mwana wa Mungu. Huyu Kuhani Mkuu wetu anaelewa kabisa unyonge wetu; yeye mwenyewe alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi. Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida. Kila kuhani mkuu ambaye huchaguliwa miongoni mwa watu hupewa jukumu la kushughulikia mambo ya Mungu kwa niaba ya watu, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi. Maadamu yeye mwenyewe ni dhaifu, anaweza kuwatendea kwa huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa. Kwa sababu hiyo anapaswa kutoa tambiko si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe. Hakuna mtu awezaye kujifanya mwenyewe kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni. Hali kadhalika naye Kristo; yeye hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimteua na kumwambia: “Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa baba yako.” Alisema pia mahali pengine: “Wewe ni kuhani milele, kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.” Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kifoni; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu. Lakini, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso. Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii, naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki. Tunayo mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu nyinyi si wepesi wa kuelewa. Kwa wakati huu nyinyi mngalipaswa kuwa waalimu tayari, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho ya mwanzo juu ya neno la Mungu. Mnahitaji maziwa badala ya chakula kigumu. Kila anayepaswa kunywa maziwa ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini. Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, waliofunzwa kwa vitendo kubainisha mema na mabaya. Basi, tuyaache nyuma yale mafundisho ya mwanzomwanzo juu ya Kristo, tusonge mbele kwa yale yaliyokomaa, na sio kuendelea kuweka msingi kuhusu kuachana na matendo ya kifo, na juu ya kumwamini Mungu; mafundisho juu ya ubatizo na kuwekewa mikono; ufufuo wa wafu na hukumu ya milele. Hilo tutafanya, Mungu akipenda. Maana watu waliokwisha kuangaziwa, wakaonja zawadi za mbinguni, wakashirikishwa Roho Mtakatifu na kuonja wema wa neno la Mungu na nguvu za ulimwengu ujao, kisha wakaiasi imani yao, haiwezekani kuwarudisha hao watubu tena. Hao wanamsulubisha tena Mwana wa Mungu kwa makusudi na kumwaibisha hadharani. Ardhi ambayo huipokea mvua inayoinyeshea mara kwa mara na kuotesha mimea ya faida kwa mkulima imebarikiwa na Mungu. Ardhi ikiota miti ya miiba na magugu, haina faida; karibu italaaniwa na Mungu na mwisho wake ni kuchomwa moto. Ingawa twasema namna hii, wapenzi wetu, tuna uhakika wa kupewa mambo mema zaidi: Yaani wokovu. Mungu hakosi haki; yeye hataisahau kazi mliyoifanya au upendo mliyoonesha kwa ajili yake katika huduma mliyowapa na mnayowapa sasa watu wake. Hamu yetu ni kwamba kila mmoja wenu aoneshe bidii hiyohiyo mpaka mwisho, ili yale mnayotumainia yapate kutimia. Hivyo msiwe wavivu, bali muwe kama wale wanaoamini na wenye uvumilivu, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Mungu alipompa Abrahamu ahadi, aliapa kwa jina lake mwenyewe, maana hakuna aliye mkuu kuliko Mungu ambaye kwa huyo angeweza kuapa. Mungu alisema: “Hakika nitakubariki na nitakupa wazawa wengi.” Abrahamu alisubiri kwa uvumilivu na hivyo akapokea kile alichoahidiwa na Mungu. Watu wanapoapa, huapa kwa mmoja aliye mkuu kuliko wao, na kiapo husuluhisha ubishi wote. Naye Mungu aliimarisha ahadi yake kwa kiapo; na kwa namna hiyo akawaonesha wazi wale aliowaahidia kwamba hatabadili nia yake. Basi, kuna vitu hivi viwili: Ahadi na kiapo, ambavyo haviwezi kubadilika na wala juu ya hivyo Mungu hawezi kusema uongo. Kwa hiyo sisi tuliokimbilia usalama kwake, tunapewa moyo wa kushikilia imara tumaini lililowekwa mbele yetu. Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo lapenya mpaka mahali patakatifu mbinguni. Yesu mwenyewe ametangulia kuingia humo kwa ajili yetu na amekuwa kuhani mkuu milele, kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki. Huyo Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme, Melkisedeki alikutana naye, akambariki, naye Abrahamu akampa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina Melkisedeki ni “Mfalme wa Uadilifu;” na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina maana ya “Mfalme wa Amani.”) Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi; haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima. Basi, mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Babu Abrahamu alimpa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyoteka nyara vitani. Tunajua pia kwamba kufuatana na sheria, wazawa wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo haki ya kuchukua sehemu moja ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao ni wazawa wa Abrahamu. Lakini huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya Mungu. Hakuna mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu kuliko yule anayebarikiwa. Tena, hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi. Twaweza, basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye wazawa wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia. Maana Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake, Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye. Kutokana na ukuhani wa Walawi, watu wa Israeli walipewa sheria. Sasa, kama huduma ya Walawi ingalikuwa kamilifu, hapangekuwa tena na haja ya kutokea ukuhani mwingine tofauti, na ambao umefuata utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki, na si ule wa Aroni. Maana ukuhani ukibadilika, ni lazima sheria nayo ibadilike. Naye Bwana wetu ambaye mambo hayo yote yanasemwa juu yake, alikuwa wa kabila lingine, na wala hakuna hata mmoja wa kabila lake aliyepata kutumikia madhabahuni akiwa kuhani. Inafahamika wazi kwamba yeye alizaliwa katika kabila la Yuda ambalo Mose hakulitaja alipokuwa anasema juu ya makuhani. Tena jambo hili ni dhahiri zaidi: Kuhani mwingine anayefanana na Melkisedeki amekwisha tokea. Yeye hakufanywa kuhani kwa sheria na maagizo ya kibinadamu, bali kwa nguvu ya uhai ambao hauna mwisho. Maana Maandiko yasema: “Wewe ni kuhani milele, kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.” Basi, ile amri ya zamani ilifutwa kwa sababu ilikuwa hafifu na isiyofaa kitu. Maana sheria ya Mose haikuweza kukamilisha jambo lolote. Lakini sasa, mahali pake pamewekwa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo tunaweza kumkaribia Mungu. Zaidi ya hayo, hapa pana kiapo cha Mungu. Wakati wale wengine walipofanywa makuhani hapakuwako kiapo. Lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia: “Bwana ameapa, wala hatabadili nia yake: ‘Wewe ni kuhani milele.’” Basi, kutokana na tofauti hii, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi. Tena: Hao makuhani wengine walikuwa wengi kwa sababu walikufa na hawakuweza kuendelea na kazi yao. Lakini Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake. Hivyo, yeye anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu. Basi, ilikuwa jambo la kufaa sana kwetu kuwa na kuhani kama huyo, mtakatifu, asiye na hatia wala dhambi ndani yake; ametenganishwa mbali na wenye dhambi, na ameinuliwa juu ya mbingu. Tofauti na makuhani wengine, yeye hahitaji kutoa tambiko kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Yeye alifanya hivyo mara moja kwa ajili ya watu wote, alipojitoa yeye mwenyewe, na hiyo yatosha kwa nyakati zote. Sheria huwateua watu walio dhaifu kuwa makuhani wakuu; lakini ahadi ya Mungu aliyoifanya kwa kiapo na ambayo imefika baada ya sheria imemteua Mwana ambaye amefanywa mkamilifu milele. Basi, jambo muhimu katika hayo tunayosema ni hili: Sisi tunaye kuhani mkuu wa namna hiyo, ambaye anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mkuu mbinguni. Yeye hutoa huduma ya kuhani mkuu mahali patakatifu katika maskani, yaani ndani ya ile hema ya kweli iliyojengwa na Bwana, siyo na binadamu. Kila kuhani mkuu ameteuliwa kumtolea Mungu zawadi na tambiko, na hivyo kuhani mkuu wetu lazima naye awe na kitu cha kutolea. Kama yeye angekuwa wa hapa duniani, asingekuwa kamwe kuhani, kwani wako makuhani wengine wanaotoa sadaka kufuatana na sheria. Huduma zao za kikuhani ni mfano tu na kivuli cha yale yaliyoko mbinguni. Maana Mose alipokuwa karibu kuitengeneza ile maskani, Mungu alimwambia: “Tengeneza kila kitu kufuatana na ule mfano uliooneshwa kule mlimani.” Lakini sasa Yesu amepewa huduma ya kikuhani iliyo bora kuliko yao, kama vile agano alilothibitisha kati ya watu na Mungu ni bora zaidi, kwani lina msingi wake katika ahadi za mambo yaliyo bora zaidi. Maana kama lile agano la kwanza halingalikuwa na dosari, hakungalikuwa na haja ya agano la pili. Lakini Mungu aliwalaumu watu wake aliposema: “Siku zinakuja, asema Bwana, ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na wa Yuda. Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na babu zao siku nilipowaongoza kwa mkono kutoka Misri. Hawakuwa waaminifu kwa agano langu; na hivyo mimi sikuwajali, asema Bwana. Hili ndilo agano nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Hakuna atakayemfundisha mwananchi mwenzake, wala atakayemwambia ndugu yake: ‘Mjue Bwana’. Maana wote, wadogo na wakubwa, watanijua mimi. Nitawasamehe makosa yao, wala sitakumbuka tena dhambi zao.” Kwa kusema juu ya agano jipya, Mungu alilichakaza lile la kwanza; na chochote kinachochakaa na kuwa kikuukuu kitatoweka karibuni. Agano la kwanza lilikuwa na taratibu zake za ibada na maskani takatifu ya duniani. Palitengenezwa hema ambayo sehemu yake ya nje iliitwa Mahali Patakatifu. Humo mlikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Nyuma ya pazia la pili, kulikuwa na hema iliyoitwa Mahali Patakatifu sana. Humo mlikuwa na madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kufukizia ubani, na sanduku la agano, ambalo lilikuwa limepakwa dhahabu pande zote, na ndani yake mlikuwa na chungu cha dhahabu kilichokuwa na mana, fimbo ya Aroni iliyokuwa imechanua majani, na vile vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa agano. Juu ya hilo sanduku kulikuwa na viumbe wenye mabawa, na mabawa yao yalitanda juu ya kiti cha rehema. Lakini sasa hatuwezi kusema kinaganaga juu ya mambo hayo. Mipango hiyo ilitekelezwa, kisha ikawa desturi kwa makuhani kuingia kila siku katika hema ya nje kutoa huduma zao. Lakini kuhani mkuu peke yake ndiye anayeingia katika lile hema la pili; naye hufanya hivyo mara moja tu kwa mwaka, na huwa amechukua damu ambayo anamtolea Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya makosa ya watu. Kutokana na taratibu hizo Roho Mtakatifu anafundisha wazi kwamba wakati ile hema ya nje ingali ipo imesimama, njia ya kuingia Mahali Patakatifu sana haijafunguliwa. Jambo hili ni mfano wa nyakati za sasa, ambapo zawadi na tambiko zinatolewa lakini haziwezi kuifanya dhamiri za wanaoabudu kuwa kamilifu, kwani haya yote yanahusika na vyakula, vinywaji na taratibu mbalimbali za kutawadha. Yote hayo ni maagizo ya njenje tu; na nguvu yake hukoma wakati Mungu atakaporekebisha vitu vyote. Lakini Kristo amekwisha fika, akiwa kuhani mkuu wa mambo yaliyo mema, ambayo sasa yamekwisha fika. Yeye anatoa huduma zake katika hema iliyo bora na kamilifu zaidi, isiyofanywa kwa mikono ya watu, yaani isiyo ya ulimwengu huu ulioumbwa. Yeye aliingia Mahali Patakatifu mara moja tu, akiwa amechukua, sio damu ya mbuzi na ng'ombe, bali amechukua damu yake yeye mwenyewe, akatupatia ukombozi wa milele. Watu waliokuwa najisi kidini waliweza kutakasika na kuwa safi waliponyunyiziwa damu ya mbuzi na ya ng'ombe pamoja na majivu ya ndama. Lakini, kwa damu ya Kristo, mambo makuu zaidi hufanyika! Kwa nguvu ya Roho wa milele, Kristo alijitolea mwenyewe tambiko kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo kifo, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai. Hivyo yeye ni mpatanishi wa agano jipya ambamo wale walioitwa na Mungu wanaweza kupokea baraka za milele walizoahidiwa. Kifo chake huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la kale. Kwa kawaida wosia hutambuliwa tu kama kifo cha yule aliyeufanya huo wosia kimethibitishwa. Wosia hauwezi kutekelezwa mpaka kumetokea kifo, kwani wosia hauna maana ikiwa mwenye kuufanya bado anaishi. Ndiyo maana hata lile agano la kwanza halikuwekwa bila damu kumwagwa. Kwanza Mose aliwatangazia watu wote amri zote kama ilivyokuwa katika sheria; kisha akachukua damu ya ndama pamoja na maji, na kwa majani ya mti wa husopo na pamba nyekundu, akakinyunyizia kile kitabu cha sheria na watu wote. Mose alisema: “Hii ni damu inayothibitisha agano mliloamriwa na Mungu mlitii.” Vilevile Mose aliinyunyizia damu ile hema na vyombo vya ibada. Naam, kadiri ya sheria karibu kila kitu chaweza kutakaswa kwa damu, na dhambi nazo zaondolewa tu ikiwa damu imemwagwa. Vitu hivi ambavyo ni mfano tu wa mambo halisi ya mbinguni, vililazimika kutakaswa kwa namna hiyo. Lakini vitu vya mbinguni huhitaji tambiko iliyo bora zaidi. Maana Kristo hakuingia Mahali Patakatifu palipojengwa kwa mikono ya watu, ambapo ni mfano tu wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni kwenyewe ambako sasa anasimama mbele ya Mungu kwa ajili yetu. Kuhani mkuu wa Wayahudi huingia Mahali Patakatifu kila mwaka akiwa na damu ya mnyama; lakini Kristo hakuingia humo ili ajitoe mwenyewe mara nyingi, maana ingalikuwa hivyo, Kristo angalipaswa kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa ulimwengu. Lakini sasa, nyakati hizi zinapokaribia mwisho wake, yeye ametokea mara moja tu kuondoa dhambi kwa kujitoa yeye mwenyewe tambiko. Basi, kama vile kila mtu hufa mara moja tu, kisha husimama mbele ya hukumu ya Mungu, vivyo hivyo Kristo naye alijitoa tambiko mara moja tu kwa ajili ya kuziondoa dhambi za wengi. Atakapotokea mara ya pili, si kwa ajili ya kupambana na dhambi, bali ni kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomngojea. Kwa vile sheria ni kivuli tu cha mambo mema yatakayokuja na si picha kamili ya mambo yale halisi, tambiko zilezile za sheria zinazotolewa mwaka hata mwaka, haziwezi kamwe kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu! Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na tambiko hizo zote zingekoma. Lakini tambiko hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao. Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi. Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: “Hukutaka tambiko wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili. Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi. Hapo nikasema: ‘Niko hapa, ee Mungu, kutimiza matakwa yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha sheria.’” Kwanza alisema: “Hutaki wala hupendezwi na tambiko, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi.” Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na sheria. Kisha akasema: “Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya matakwa yako.” Hivyo Mungu alibatilisha tambiko za zamani na mahali pake akaweka tambiko nyingine moja. Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza matakwa ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile tambiko ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha. Kila kuhani Myahudi hutoa huduma yake ya ibada ya kila siku na kutoa tambiko zilezile mara nyingi, tambiko ambazo haziwezi kuondoa dhambi. Lakini Kristo alitoa tambiko moja kwa ajili ya dhambi, tambiko ifaayo milele, kisha, akaketi upande wa kulia wa Mungu, anangoja maadui zake wafanywe kama kibao chini ya miguu yake. Basi, kwa tambiko yake moja, amewafanya kuwa wakamilifu milele wote wale wanaotakaswa dhambi zao. Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema: “Hili ndilo agano nitakalofanya nao, siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao.” Kisha akaongeza kusema: “Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu.” Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa tambiko za kuondoa dhambi. Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu. Yeye ametufungulia njia mpya, njia ya uhai, kupitia lile pazia, yaani mwili wake mwenyewe. Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa kutokana na dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi. Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu. Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema. Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, siku ile ya Bwana inakaribia. Maana, tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna tambiko iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi. Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza wote wanaompinga. Mtu yeyote asiyetii sheria ya Mose, huuawa bila huruma kukiwa na ushahidi wa watu wawili au watatu. Je, mtu yule anayempuuza Mwana wa Mungu na kuidharau damu ya agano la Mungu iliyomtakasa, mtu anayemtukana Roho wa Mungu, anastahili kupata adhabu kali ya namna gani? Maana tunamfahamu yule aliyesema, “Mimi nitalipiza kisasi, mimi nitalipiza,” na ambaye alisema pia, “Bwana atawahukumu watu wake.” Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha mno! Kumbukeni yaliyotokea siku zile za kwanza mlipoangaziwa mwanga wa Mungu. Ingawa siku zile mlipatwa na mateso mengi, nyinyi mlistahimili. Mara nyingine mlitukanwa na kufedheheshwa hadharani; mara nyingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa namna hiyohiyo. Mlishiriki mateso ya wafungwa na mliponyanganywa mali yenu mlistahimili kwa furaha, maana mlijua kwamba mnayo mali bora zaidi na ya kudumu milele. Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatia tuzo kubwa. Mnahitaji kuwa na uvumilivu ili muweze kutimiza matakwa ya Mungu na kupokea kile alichoahidi. Maana kama yasemavyo Maandiko: “Bado kidogo tu, na yule anayekuja, atakuja, wala hatakawia. Lakini mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi; walakini akirudi nyuma, mimi sitapendezwa naye.” Basi, sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tumo na wale wanaoamini na kuokolewa. Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona. Maana wazee wa kale walipata kibali cha Mungu kwa sababu ya imani yao. Kwa imani sisi tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu; vitu vinavyoonekana kutoka vitu visivyoonekana. Kwa imani Abeli alimtolea Mungu tambiko iliyokuwa bora kuliko ile ya Kaini. Kwa imani yake alikubaliwa na Mungu kuwa mwadilifu; Mungu mwenyewe alizikubali sadaka zake. Kwa imani yake ingawa alikufa, bado ananena. Kwa imani Henoki alichukuliwa na Mungu, asipate kufa. Hakuonekana tena kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Maandiko yasema kwamba kabla ya kuchukuliwa kwake, yeye alikuwa amempendeza Mungu. Basi, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa maana kila mtu anayemwendea Mungu ni lazima aamini kwamba Mungu yuko, na kwamba huwatuza wale wanaomtafuta. Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hayakuwa yameonekana bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani. Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama. Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile. Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga. Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri. Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani. Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani. Watu wanaosema mambo kama hayo, huonesha wazi kwamba wanaitafuta nchi yao wenyewe. Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi walikotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko. Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Ndio maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji. Kwa imani Abrahamu alimtoa tambiko mwanawe Isaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa tambiko mwanawe wa pekee, ingawa Mungu alikuwa amemwambia: “Wazawa wako watatokana na Isaka.” Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu; na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanawe kutoka kwa wafu. Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau, wapate baraka zitakazokuja baadaye. Kwa imani Yakobo alipokuwa karibu kufa, aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiegemea kichwa cha ile fimbo yake. Kwa imani Yosefu alipokuwa karibu kufa, alinena juu ya kutoka kwa Waisraeli katika nchi ya Misri, na pia akawaachia maagizo kuhusu mifupa yake. Kwa imani wazazi wa Mose walimficha huyo mtoto kwa muda wa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Walimwona kuwa ni mtoto mzuri, wala hawakuiogopa amri ya mfalme. Kwa imani Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. Aliona ni afadhali kuteseka pamoja na watu wa Mungu kuliko kufurahia raha ya dhambi kwa kitambo kidogo. Alitambua kwamba kuteseka kwa ajili ya Kristo kuna faida kubwa kuliko utajiri wote wa nchi ya Misri, maana alikuwa anatazamia tuzo la baadaye. Kwa imani Mose alihama kutoka nchi ya Misri bila kuogopa hasira ya mfalme; na wala hakurudi nyuma, kwani alikuwa kama mtu aliyemwona yule Mungu asiyeonekana. Kwa imani aliadhimisha siku ya Pasaka, akaamuru damu inyunyizwe juu ya milango, ili yule Malaika Mwangamizi asiwaue wazaliwa wa kwanza wa Israeli. Kwa imani watu wa Israeli walivuka bahari ya Shamu kana kwamba ilikuwa nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo walikufa maji. Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kuta hizo kwa siku saba. Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi. Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gideoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samueli na manabii. Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba, walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga, walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita, wakashinda majeshi ya kigeni. Na, wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao wakiwa wamefufuliwa. Baadhi yao walikataa kufunguliwa, wakateswa mpaka kufa ili wapate kufufuliwa na kuingia katika maisha bora zaidi. Wengine walidhihakiwa na kupigwa mijeledi, na wengine walifungwa minyororo na kutupwa gerezani. Walipigwa mawe, walipasuliwa vipandevipande, waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa watu maskini, walioteswa na kudhulumiwa. Ulimwengu haukustahili kuwa na watu hao. Walitangatanga jangwani na milimani, wakaishi katika mashimo na mapango ya ardhi. Watu hawa wote walionekana kuwa mashujaa kwa sababu ya imani yao. Hata hivyo, hawakupokea yale ambayo Mungu aliwaahidi, maana Mungu alikuwa ameazimia mpango ulio bora zaidi kwa ajili yetu; yaani wao wangeufikia ukamilifu wakiwa pamoja nasi. Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotungangania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu. Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kuijali aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu. Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa. Maana katika kupambana na dhambi, nyinyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu. Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja nyinyi kuwa wanawe? “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usife moyo anapokukanya. Maana Bwana humpa nidhamu kila anayempenda, humwadhibu kila anayekubali kuwa mwanawe.” Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea nyinyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake? Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, nyinyi si wanawe, bali ni wana haramu. Zaidi ya hayo, sisi tunawaheshimu wazazi wetu waliotuzaa hata wanapotuadhibu. Basi, tunapaswa kumtii zaidi Baba yetu wa kiroho ili tupate kuishi. Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake. Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili. Basi, inueni mikono yenu inayolegea na kuimarisha magoti yenu yaliyo dhaifu. Endeleeni kutembea katika njia iliyonyoka, ili kile kilicholemaa kisiumizwe, bali kiponywe. Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote. Ishini maisha ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama hayo. Jitahidini sana mtu yeyote asije akapoteza neema ya Mungu. Muwe waangalifu ili mti mchungu usizuke kati yenu na kuwaua wengi kwa sumu yake. Jihadharini ili miongoni mwenu pasiwe na mtu mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, aliyeuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mlo mmoja. Nyinyi mnafahamu kwamba hata alipotaka kuipata tena ile baraka iliyokuwa yake, alikataliwa, maana hakupata tena nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi. Nyinyi hamkuwasili mlimani Sinai, ambao unaweza kushikika kama walivyofanya watu wa Israeli; hamkufika kwenye moto uwakao, penye giza, tufani, mvumo wa tarumbeta na sauti ya maneno. Wale waliosikia sauti hiyo waliomba wasisikie tena neno lingine, kwani hawakuweza kustahimili amri iliyotolewa: “Atakayegusa mlima huu, hata kama ni mnyama, atapigwa mawe.” Hayo yote yalionekana ya kutisha mno, hata Mose akasema, “Naogopa na kutetemeka.” Lakini nyinyi mmefika katika mlima wa Siyoni, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika malaika kwa maelfu. Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa wakamilifu. Mmefika kwa Yesu ambaye ni mpatanishi katika agano jipya, na ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema kuliko ile ya Abeli. Basi, jihadharini msije mkakataa kumsikiliza huyo anayesema nanyi. Kama wale waliokataa kumsikiliza yule aliyewaonya hapa duniani hawakuokoka, sisi tutawezaje kuokoka kama tukikataa kumsikiliza yule anayetuonya kutoka mbinguni? Wakati ule sauti ilitetemesha nchi, lakini sasa ameahidi: “Nitatetemesha nchi tena, lakini si nchi tu bali pia mbingu.” Neno hili: “Tena” linatuonesha kwamba vitu vyote vilivyoumbwa vitatetemeshwa na kutoweka ili vibaki vile visivyotetemeshwa. Sisi basi, na tushukuru, kwani tunapokea ufalme usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu; maana Mungu wetu kweli ni moto mkali unaoteketeza. Endeleeni kupendana kindugu. Msisahau kuwakaribisha wageni; maana kwa kufanya hivyo watu wengine walipata kuwakaribisha malaika bila kujua. Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao. Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao. Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu. Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi. Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” Ndiyo maana tunathubutu kusema: “Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?” Wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni neno la Mungu. Fikirini juu ya mwenendo wao, mkaige imani yao. Yesu Kristo ni yuleyule jana, leo na milele. Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata. Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi hawana haki ya kula vitu vyake. Kuhani mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa tambiko kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji. Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake. Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja. Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu tambiko ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa kwa midomo inayoliungama jina lake. Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo tambiko zinazompendeza Mungu. Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu. Mtuombee na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima. Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo. Mungu amemfufua katika wafu Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele. Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina. Basi, ndugu, nawasihi mpokee kwa utulivu ujumbe huu wa kuwatieni moyo. Hii ni barua fupi tu ambayo nimewaandikieni. Napenda kuwajulisheni kwamba ndugu yetu Timotheo amekwisha funguliwa gerezani. Kama akifika hapa mapema, nitakuja naye nitakapokuja kwenu. Wasalimuni viongozi wenu wote pamoja na watu wa Mungu! Ndugu wa Italia wanawasalimuni. Tunawatakieni nyote neema ya Mungu. Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salamu! Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu. Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote. Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu. Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo. Kwa hiyo mtu aliye na mashaka, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote, asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana. *** Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza, naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini. Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake. Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili, atapewa tuzo la uhai ambalo Mungu aliwaahidi wale wanaompenda. Kama mtu akijaribiwa, asiseme: “Ninajaribiwa na Mungu.” Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote. Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya. Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike! Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe katika nafasi ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake. Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini si mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika. Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea lile neno lililopandwa mioyoni mwenu, ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu. Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo. Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya. Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe. Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu. Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe. Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu. Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: “Keti hapa mahali pazuri,” na kumwambia yule maskini: “Wewe, simama huko,” au “Keti hapa sakafuni miguuni pangu,” je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea ufalme aliowaahidia wale wanaompenda. Lakini nyinyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamiza na kuwapeleka mahakamani? Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa? Kama mnaitimiza ile sheria ya ufalme kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe”, mtakuwa mnafanya vema kabisa. Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo sheria inawahukumu nyinyi kuwa mna hatia. Anayevunja amri mojawapo ya sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja sheria yote. Maana yuleyule aliyesema: “Usizini,” alisema pia “Usiue.” Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini, lakini umeua, wewe umeivunja sheria. Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru. Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu. Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa? Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula. Yafaa kitu gani nyinyi kuwaambia hao: “Nendeni salama mkaote moto na kushiba,” bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha? Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa. Lakini mtu anaweza kusema: “Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!” Haya! Nioneshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonesha imani yangu kwa matendo yangu. Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu. Mpumbavu wee! Je, wataka kuoneshwa kwamba imani bila matendo imekufa? Je, Abrahamu babu yetu alipataje kukubaliwa kuwa mwadilifu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa tambiko mwanawe Isaka juu ya madhabahu. Waona, basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake. Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: “Abrahamu alimwamini Mungu, na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki ya Mungu.” Mnaona, basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake, na si kwa imani peke yake. Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine. Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa. Ndugu zangu, wengi wenu msiwe waalimu. Kama mjuavyo, sisi waalimu tutapata hukumu kubwa zaidi kuliko wengine. Lakini kama mtu hakosi katika usemi wake, basi, huyo ni mkamilifu, na anaweza kutawala nafsi yake yote. Sisi huwatia farasi lijamu kinywani mwao ili watutii; na kwa njia hiyo twaweza kuwaongoza kokote tunakotaka. Meli nazo pia, ingawa ni kubwa sana, na husukumwa na upepo mkali, huweza kugeuzwa kwa usukani mdogo sana, zikaelekea kokote nahodha anakotaka. Vivyo hivyo, ulimi, ingawa ni kiungo kidogo cha mwili, hujisifia makuu sana. Moto mdogo waweza kuteketeza msitu mkubwa. Hali kadhalika ulimi ni kama moto. Umejaa maovu chungu nzima, unayo nafasi yake katika miili yetu na hueneza ubaya katika nafsi zetu zote. Huteketeza maisha yetu yote kwa moto utokao Jehanamu kwenyewe. Binadamu anaweza kuwafuga wanyama, na amefaulu kufuga viumbe vyote — wanyama wa mwituni, ndege, nyoka na viumbe vya baharini. Lakini hakuna mtu aliyefaulu kuufuga ulimi. Ulimi ni kitu kiovu, hakitawaliki, na kimejaa sumu inayoua. Kwa ulimi sisi twamshukuru Bwana na Baba yetu. Kwa ulimi huhuo twawalaani watu, watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu. Maneno ya kubariki na ya kulaani hutoka katika kinywa kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapaswi kuwa hivyo. Je, chemchemi moja yaweza kutoa maji matamu na maji machungu pamoja? Ndugu zangu, je, mtini waweza kuzaa zeituni? Au, mzabibu waweza kuzaa tini? Chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu. Je, ni nani mwenye hekima na akili miongoni mwenu? Basi, aoneshe jambo hilo kwa mwenendo wake mzuri na kwa matendo yake mema yanayofanyika kwa unyenyekevu na hekima. Lakini ikiwa mioyo yenu imejaa wivu, chuki na ubinafsi, basi, msijisifu na kusema uongo dhidi ya ukweli. Hekima ya namna hiyo haitoki juu mbinguni; hekima hiyo ni ya ulimwengu, na ya kidunia, tena ni ya kishetani. Maana popote palipo na wivu na ubinafsi, hapo pana fujo na kila aina ya uovu. Lakini hekima itokayo juu mbinguni, kwanza ni safi; inapenda amani, upole na huwajali watu; imejaa huruma na huzaa matunda ya matendo mema; haina ubaguzi wala unafiki. Uadilifu ni mazao ya mbegu ambazo wapenda amani hupanda katika amani. Mapigano na ugomvi wote kati yenu vinatoka wapi? Hutoka katika tamaa zenu mbaya ambazo hupigana daima ndani yenu. Mnatamani vitu na kwa vile hamvipati mko tayari kuua; mwatamani sana kupata vitu, lakini hamvipati; hivyo mnagombana na kupigana. Hampati kile mnachotaka kwa sababu hamkiombi kwa Mungu. Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu. Nyinyi ni watu msio na uaminifu kama wazinzi. Je, hamjui kwamba kuwa rafiki wa ulimwengu ni kuwa adui wa Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa ulimwengu anajifanya adui wa Mungu. Msifikiri kwamba Maandiko Matakatifu yamesema maneno ya bure, yanaposema: “Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu ana wivu mkubwa.” Lakini, neema tunayopewa na Mungu ina nguvu zaidi; kama yasemavyo Maandiko: “Mungu huwapinga wenye majivuno lakini huwapa neema wanyenyekevu.” Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Ibilisi naye atawakimbieni. Mkaribieni Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenu enyi wakosefu! Safisheni mioyo yenu enyi wanafiki! Oneni huzuni, lieni na kuomboleza; kicheko chenu na kiwe kilio; na furaha yenu iwe huzuni kubwa. Nyenyekeeni mbele ya Bwana, naye atawainueni. Ndugu, msilaumiane nyinyi kwa nyinyi. Anayemlaumu ndugu yake na kumhukumu, huyo huilaumu na kuihukumu sheria. Kama ukiihukumu sheria, basi, wewe huitii sheria, bali waihukumu. Mungu peke yake ndiye mwenye kuweka sheria na kuhukumu. Ni yeye peke yake anayeweza kuokoa na kuangamiza. Basi, wewe ni nani hata umhukumu binadamu mwenzako? Basi, sasa sikilizeni nyinyi mnaosema: “Leo au kesho tutakwenda katika mji fulani na kukaa huko mwaka mzima tukifanya biashara na kupata faida.” Nyinyi hamjui hata maisha yenu yatakavyokuwa kesho! Nyinyi ni kama ukungu unaotokea kwa muda mfupi tu na kutoweka tena. Mngalipaswa kusema: “Bwana akitujalia tutaishi na tutafanya hiki au kile.” Lakini sasa mwajivuna na kujigamba; majivuno ya namna hiyo ni mabaya. Basi, mtu ambaye hafanyi lile jambo jema analojua kwamba anapaswa kulifanya, anatenda dhambi. Na sasa sikilizeni enyi matajiri! Lieni na kuomboleza kwa sababu ya taabu zitakazowajieni. Mali zenu zimeoza, na nguo zenu zimeliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha vimeota kutu, na kutu hiyo itakuwa ushahidi dhidi yenu, nayo itakula miili yenu kama vile moto. Nyinyi mmejirundikia mali katika siku hizi za mwisho! Hamkuwalipa mishahara watumishi waliofanya kazi katika mashamba yenu. Sikilizeni malalamiko yao! Kilio cha hao wanaovuna mashamba yenu kimefika masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmeishi duniani maisha ya kujifurahisha na ya anasa. Mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. Mmemhukumu na kumuua mtu asiye na hatia, naye hakuwapingeni! Basi, ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima anavyongoja kwa subira mimea yake itoe mavuno ya thamani. Yeye hungojea kwa subira mvua za masika na za vuli. Nanyi pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake Bwana inakaribia. Ndugu zangu, msinung'unikiane nyinyi kwa nyinyi msije mkahukumiwa na Mungu. Hakimu yu karibu, tayari kuingia. Ndugu, mkitaka kuona mfano wa subira na uvumilivu katika mateso, fikirini juu ya manabii ambao walinena kwa jina la Bwana. Tunawaita hao wenye heri kwa sababu walivumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wa Yobu, na mnajua jinsi Bwana alivyomtendea mwishoni. Maana Bwana amejaa huruma na rehema. Zaidi ya hayo yote, ndugu zangu, msiape kwa mbingu, wala kwa dunia, wala kwa kitu kingine chochote. Semeni “Ndiyo” kama maana yenu ni ndiyo, na “La” kama maana yenu ni la, na hapo hamtahukumiwa na Mungu. Je, pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. Je, yuko mgonjwa kati yenu? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa, nao watamwombea na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Wakiomba kwa imani mgonjwa ataponyeshwa; Bwana atampatia nafuu, na dhambi alizotenda zitaondolewa. Basi, ungamanieni dhambi zenu, na ombeaneni, ili mpate kuponywa. Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda mengi. Elia alikuwa binadamu kama sisi. Aliomba kwa moyo mvua isinyeshe, nayo haikunyesha nchini kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. Kisha akaomba tena, mvua ikanyesha kutoka angani na nchi ikatoa mazao yake. Ndugu zangu, mmoja wenu akipotoka kuhusu ukweli, na mwingine akamrudisha, fahamuni kwamba, huyo anayemrudisha mwenye dhambi kutoka njia yake ya upotovu, ataiokoa roho yake kutoka kifo, na dhambi nyingi zitaondolewa. Mimi Petro, mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi wateule wa Mungu Baba, ambao mmetawanyika na mnaishi kama wakimbizi huko Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithunia. Mungu Baba aliwateua nyinyi kufuatana na kusudi lake, na mmefanywa watakatifu na Roho, mpate kumtii Yesu Kristo na kusafishwa kwa damu yake. Nawatakieni neema na amani tele. Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Ametujalia tumaini lenye uhai, na hivyo tunatazamia kupata baraka zile ambazo Mungu aliwawekea watu wake. Mungu amewawekeeni baraka hizo mbinguni ambako haziwezi kuoza, au kuharibika, au kufifia. Hizo zitakuwa zenu nyinyi ambao kwa imani mnalindwa salama kwa nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu ambao uko tayari kufunuliwa mwishoni mwa nyakati. Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka, majaribio ambayo shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe, ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu, ambayo ni ya thamani kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa. Nyinyi mnampenda, ingawaje hamjamwona, na mnamwamini, ingawa hammwoni sasa. Hivyo, mnafurahi kwa furaha tukufu isiyoelezeka, kwa sababu mnapokea wokovu wa roho zenu ambao ni lengo la imani yenu. Manabii walipeleleza na kufanya uchunguzi juu ya wokovu huo, wakabashiri juu ya neema hiyo ambayo nyinyi mngepewa. Walijaribu kujua nyakati na mazingira ya tukio hilo, yaani wakati alioudokezea Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, akibashiri juu ya mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaofuata. Mungu aliwafunulia kwamba wakati walipokuwa wanasema juu ya hayo mambo ambayo nyinyi mmekwisha sikia sasa kutoka kwa wale wajumbe waliowatangazieni Habari Njema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni, hiyo kazi yao haikuwa kwa faida yao wenyewe, bali kwa ajili yenu. Hayo ndiyo mambo ambayo hata malaika wangependa kuyafahamu. Kwa hiyo, basi, muwe tayari kabisa, na kukesha. Wekeni tumaini lenu lote katika neema ile mtakayopewa wakati Yesu Kristo atakapoonekana! Kama watoto wa Mungu wenye utii, msikubali kamwe kufuata tena tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mlipokuwa wajinga. Bali mnapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote, kama vile yule aliyewaiteni ni mtakatifu. Maandiko yasema: “Muwe watakatifu, kwa kuwa mimi alivyo mtakatifu.” Mnapomtaja Mungu, nyinyi humwita Baba. Basi, jueni kwamba yeye humhukumu kila mmoja kadiri ya matendo yake, bila ubaguzi. Hivyo tumieni wakati wenu uliowabakia hapa ugenini katika kumcha Mungu. Maana mnajua kwamba nyinyi mlikombolewa katika mwenendo wenu usiofaa ambao mliupokea kutoka kwa wazee wenu. Lakini hamkukombolewa kwa vitu vyenye kuharibika: Kwa fedha na dhahabu; bali kwa damu ya thamani ya Kristo, ambaye alikuwa kama mwanakondoo asiye na dosari wala doa. Yeye alikuwa ameteuliwa na Mungu kabla ya ulimwengu kuumbwa, akafunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. Kwa njia yake, mnamwamini Mungu aliyemfufua kutoka kwa wafu na kumpa utukufu; na hivyo imani na matumaini yenu yako kwa Mungu. Maadamu sasa, kwa kuutii ukweli, nyinyi mmezitakasa roho zenu na kuwapenda wenzenu bila unafiki, basi, pendaneni kwa moyo wote. Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, nyinyi mmezaliwa upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele. Kama Maandiko yasemavyo: “Kila binadamu ni kama majani, na utukufu wake wote ni kama ua la majani. Majani hunyauka na maua huanguka. Lakini neno la Bwana hudumu milele.” Neno hilo ni hiyo Habari Njema mliyohubiriwa. Basi, acheni uovu wote; uongo, unafiki, wivu na maneno ya kashfa visiweko tena. Kama vile watoto wachanga wanavyotamani maziwa, nanyi pia mnapaswa kuwa na hamu ya maziwa halisi ya kiroho, ili kwa nguvu yake mpate kukua na kukombolewa. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mmegundua kwamba Bwana ni mwema.” Basi, mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa na watu; lakini mbele ya Mungu ni jiwe teule na la thamani kubwa. Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya kiroho ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea tambiko za kiroho zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Tazama! Naweka jiwe huko Siyoni, jiwe la msingi, teule na la thamani. Mtu atakayemwamini huyo hataaibishwa.” Kwenu nyinyi mnaoamini, jiwe hilo ni la thamani kubwa; lakini kwa wale wasioamini, “Jiwe walilolikataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.” Tena Maandiko yasema: “Jiwe hilo ni jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuwaangusha watu.” Watu hujikwaa kwa sababu hawauamini ule ujumbe; na ndivyo walivyopangiwa tangu mwanzo. Lakini nyinyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu. Wakati mmoja nyinyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa nyinyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmepokea huruma. Wapenzi wangu, nawasihi nyinyi kama wageni na wakimbizi hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho. Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu siku ya kuja kwake. Basi, jiwekeni chini ya mamlaka yote ya kibinadamu, kwa ajili ya Bwana: Utii kwa mfalme aliye mtawala mkuu, utii kwa wakuu wa mikoa ambao wameteuliwa naye kuwaadhibu wahalifu na kuwasifu watendao mema. Maana Mungu anataka muweze kuyakomesha maneno ya kijinga ya watu wasio na akili kwa matendo mema mnayofanya. Ishini kama watu huru; lakini msiutumie uhuru wenu kuuficha ubaya, bali ishini kama watumishi wa Mungu. Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu zenu waamini, mcheni Mungu, mheshimuni mfalme. Enyi watumishi wa nyumbani, watiini wakuu wenu kwa heshima yote, wawe wema na wapole au wenye kuchukiza. Maana kama mnavumilia maumivu ya mateso msiyostahili kwa sababu mwajua kwamba Mungu anataka hivyo, basi Mungu atawafadhili. Maana, mtapata tuzo gani mkivumilia mapigo mnayostahili kwa sababu ya makosa yenu? Lakini kama mnavumilia mateso hata ingawa mmetenda mema, Mungu atawapeni baraka kwa ajili hiyo. Hayo ndiyo mliyoitiwa; maana Kristo mwenyewe aliteseka kwa ajili yenu, akawaachieni mfano, ili mfuate mwenendo wake. Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake. Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki. Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya msalaba, tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa majeraha yake, nyinyi mmeponywa. Nyinyi mlikuwa kama kondoo waliokuwa wamepotea; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mlinzi wa roho zenu. Nanyi wake, jiwekeni chini ya mamlaka ya waume zenu, ili kama wako waume wowote wasioamini neno la Mungu, wapate kuamini kwa kuuona mwenendo wenu. Haitakuwa lazima kwenu kusema neno, kwani wataona jinsi mwenendo wenu ulivyo safi na wa kumcha Mungu. Katika kujipamba kwenu msitegemee mambo ya njenje, kama vile mitindo ya kusuka nywele, kujivalia vitu vya dhahabu na nguo maridadi. Bali, uzuri wenu unapaswa kutokana na hali ya ndani ya utu wa kweli, uzuri usioharibika wa wema na utulivu wa roho, ambao ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu. Ndivyo walivyojipamba hapo kale wanawake waadilifu waliomtumainia Mungu; walijiweka chini ya mamlaka ya waume zao. Sara kwa mfano alimtii Abrahamu na kumwita yeye bwana. Nyinyi mmekuwa sasa binti zake kama mkitenda mema bila kuogopa tisho lolote. Kadhalika nanyi waume, katika kuishi na wake zenu mnapaswa kutambua kwamba wao ni dhaifu na hivyo muwatendee kwa heshima; maana nao pia watapokea pamoja nanyi zawadi ya uhai anaowapeni Mungu. Hapo sala zenu hazitatiliwa kizuizi. Mwisho nasema hivi: Mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikira moja; mnapaswa kupendana kindugu, kuwa wapole na wanyenyekevu nyinyi kwa nyinyi. Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana nyinyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Anayetaka kufurahia maisha, na kuona siku za fanaka, ajizuie asiseme mabaya aepe kusema uongo. Ajiepushe na uovu, atende mema, atafute amani na kuizingatia. Maana Bwana huwatazama kwa wema waadilifu na kuzisikiliza sala zao. Lakini huwapa kisogo watu watendao maovu.” Ni nani atakayeweza kuwadhuru nyinyi kama mkizingatia kutenda mema? Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi. Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu, lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima. Muwe na dhamiri njema, kusudi mnapotukanwa, wale wanaosema ubaya juu ya mwenendo wenu mwema kama Wakristo, waone aibu. Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, kama Mungu akipenda, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu. Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke nyinyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho; na kwa maisha yake ya kiroho alikwenda kuwahubiria wale roho waliokuwa kifungoni. Hao ndio wale waliokataa kumtii Mungu alipowangoja kwa saburi wakati Noa alipokuwa anatayarisha ile safina. Ndani ya chombo hicho ni watu wachache tu, yaani watu wanane, waliookolewa katika maji, ambayo yalikuwa mfano wa ubatizo unaowaokoa nyinyi sasa. Ubatizo si shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Huwaokoeni kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi. Maadamu Kristo aliteseka kimwili, nanyi pia mnapaswa kujiimarisha kwa nia hiyo yake; maana mtu akisha teseka kimwili hahusiki tena na dhambi. Tangu sasa, basi, maisha yaliyowabakia kuishi hapa duniani yanapaswa kuongozwa na matakwa ya Mungu, sio na tamaa za kibinadamu. Wakati uliopita mlikuwa na muda mrefu wa kufanya mambo wanayofanya watu wasiomjua Mungu. Mliishi maisha ya anasa, ubinafsi, ulevi, ugomvi, kunywa mno na ya ibada haramu za sanamu. Sasa, watu hao wasiomjua Mungu wanashangaa wanapoona kwamba hamwandamani nao tena katika hali ya kuishi vibaya, na hivyo wanawatukaneni. Lakini watapaswa kutoa hoja juu ya jambo hilo mbele yake Mungu aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa! Ndiyo maana Habari Njema ilihubiriwa hata kwa hao waliokufa, ili baada ya kuhukumiwa katika maisha yao ya kimwili kama wengine, waishi kwa ajili ya Mungu kwa njia ya Roho. Mwisho wa vitu vyote umekaribia. Kwa hiyo mnapaswa kuwa na utaratibu na kukesha ili muweze kusali. Zaidi ya yote pendaneni kwa moyo wote, maana upendo hufunika dhambi nyingi. Muwe na ukarimu nyinyi kwa nyinyi bila kunung'unika. Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine kama wakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu. Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina. Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida. Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili muweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa. Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa nanyi. Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu ambaye anapaswa kuteseka kwa sababu ni mwuaji, mwizi, mhalifu au mwovu. Lakini kama mtu akiteseka kwa sababu ni Mkristo, basi, asione aibu, bali amtukuze Mungu, kwa sababu mtu huyo anaitwa kwa jina la Kristo. Wakati wa hukumu umefika, na hukumu hiyo inaanza na watu wake Mungu mwenyewe. Ikiwa hukumu hiyo inaanzia kwetu sisi, basi, mwisho wake utakuwa namna gani kwa wale wasioamini Habari Njema ya Mungu? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa; itakuwaje basi, kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi?” Kwa hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa. Mimi mzee miongoni mwenu wazee wenzangu, mimi ambaye nilishuhudia mateso ya Kristo na kushiriki ule utukufu utakaofunuliwa, nawasihini mlichunge lile kundi la Mungu mlilokabidhiwa; mlitunze si kwa kulazimika, bali kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo si kwa tamaa ya fedha, bali kwa moyo wenu wote. Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa hilo kundi. Na wakati Mchungaji Mkuu atakapotokea, nyinyi mtapokea taji ya utukufu isiyofifia. Kadhalika nanyi vijana mnapaswa kujiweka chini ya mamlaka ya wazee. Nyinyi nyote mnapaswa kuwa na unyenyekevu mpate kutumikiana; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwajalia neema wanyenyekevu.” Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa enzi wa Mungu, ili awainue wakati ufaao. Mwekeeni matatizo yenu yote, maana yeye anawatunzeni. Muwe macho; kesheni! Maana adui yenu, Ibilisi, huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mawindo. Muwe imara katika imani na kumpinga, mkijua kwamba ndugu zenu pote duniani wanapatwa na mateso hayohayo. Lakini mkisha teseka muda mfupi, Mungu aliye asili ya neema yote na ambaye anawaiteni kuushiriki utukufu wake wa milele katika kuungana na Kristo, yeye mwenyewe atawakamilisheni na kuwapeni uthabiti, nguvu na msingi imara. Kwake yawe mamlaka milele! Amina. Nimewaandikieni barua hii fupi kwa msaada wa Silwano, ndugu ambaye namjua na kumwamini. Nataka kuwapeni moyo na kushuhudia kwamba jambo hili ni neema ya Mungu kweli. Kaeni imara katika neema hiyo. Jumuiya ya wenzenu walioteuliwa na Mungu hapa Babuloni wanawasalimuni. Vilevile mwanangu Marko anawasalimuni. Salimianeni kwa ishara ya upendo wa Kikristo. Nawatakieni amani nyinyi mlio wake Kristo. Mimi Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi ambao, kwa wema wake Mungu wetu na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani kuu tuliyojaliwa sisi. Nawatakieni neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe. Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na kuishiriki hali yake ya kimungu. Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza imani yenu kwa fadhila, fadhila yenu kwa elimu, elimu yenu kwa kuwa na kiasi, kuwa na kiasi kwa uvumilivu, uvumilivu wenu kwa uchaji wa Mungu, uchaji wenu kwa urafiki wa kindugu, na urafiki wenu wa kindugu kwa mapendo. Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha takaswa dhambi zake za zamani. Kwa hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka kamwe. Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu na mko imara katika ukweli mlioupokea. Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya. Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi. Basi, nitajitahidi kusudi baada ya kufariki kwangu mweze kuyakumbuka mambo haya kila wakati. Wakati tulipowafundisheni juu ya ukuu wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, hatukutegemea hadithi tupu zisizo na msingi. Sisi tuliuona utukufu wake kwa macho yetu wenyewe. Sisi tulikuwapo wakati alipopewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba, wakati sauti ilipomjia kutoka kwake yeye aliye Utukufu Mkuu, ikisema: “Huyu ni Mwanangu mpenzi ambaye nimependezwa naye.” Tena, sisi wenyewe tulisikia sauti hiyo kutoka mbinguni wakati tulipokuwa pamoja naye juu ya ule mlima mtakatifu. Tena, ujumbe wa manabii watuthibitishia jambo hilo; nanyi mwafanya vema kama mkiuzingatia, maana ni kama taa inayoangaza mahali penye giza mpaka siku ile itakapopambazuka na mwanga wa nyota ya asubuhi utakapong'ara mioyoni mwenu. Zaidi ya hayo, lakini, kumbukeni kwamba hakuna mtu yeyote awezaye kufafanua mwenyewe unabii ulio katika Maandiko Matakatifu. Maana hakuna ujumbe wa kinabii unaotokana na matakwa ya binadamu, bali watu walitoa unabii wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Palitokea manabii wa uongo kati ya watu, na vivyo hivyo waalimu wa uongo watatokea kati yenu. Watu hao wataingiza mafundisho maharibifu na kumkana Bwana aliyewakomboa, na kwa njia hiyo watasababisha ghafla maangamizi yao wenyewe. Tena watu wengi watazifuata hizo njia zao mbaya, na kwa sababu yao wengine wataipuuza njia ya ukweli. Kwa tamaa yao mbaya watajipatia faida kwa kuwaambieni hadithi za uongo. Lakini kwa muda mrefu sasa Hakimu wao yuko tayari, na Mwangamizi wao yuko macho! Malaika walipotenda dhambi, Mungu hakuwahurumia, bali aliwatupa katika moto wa Jehanamu ambako wamefungwa wakingojea siku ile ya hukumu. Mungu hakuihurumia dunia ya hapo kale, bali alileta gharika kuu juu ya nchi ile ya watu wasiomcha Mungu; lakini Noa ambaye alihubiri uadilifu, Mungu alimwokoa pamoja na watu wengine saba. Mungu aliiadhibu miji ya Sodoma na Gomora, akaiteketeza kwa moto, akaifanya iwe mfano wa mambo yatakayowapata watu wasiomcha Mungu. Alimwokoa Loti, mtu mwema, ambaye alisikitishwa sana na mwenendo mbaya wa watu hao waasi. Loti aliishi miongoni mwa watu hao, na kwa siku nyingi moyo wake ulikuwa katika wasiwasi mkuu aliposikia matendo yao maovu. Kwa hiyo, basi, Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa katika majaribu watu wanaomcha Mungu, na jinsi ya kuwaweka waovu katika adhabu hadi siku ile ya hukumu, hasa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kupuuza mamlaka. Watu hao ni wakaidi na wenye majivuno, huvitukana na hawaviheshimu viumbe vitukufu vya juu. Lakini malaika ambao wana uwezo na nguvu kuliko hao waalimu wa uongo, hawawashtaki na kuwatukana hao mbele ya Bwana. Watu hao ambao hutukana chochote kile wasichoelewa, ni sawa na wanyama wasio na akili ambao huzaliwa na baadaye hukamatwa na kuchinjwa! Wataangamizwa kutokana na uharibifu wao wenyewe, na watalipwa mateso kwa mateso ambayo wameyasababisha. Furaha yao ni kufanya, tena mchana kabisa, chochote kinachotosheleza anasa zao za mwili. Hao ni fedheha na aibu tupu kwa jumuiya yenu wakati wanapojiunga nanyi katika karamu zenu, hali wakifurahia njia zao za udanganyifu. Macho yao yamejaa uzinzi na uwezo wao wa kutenda dhambi hauna kikomo. Huwaongoza watu walio dhaifu mpaka mitegoni. Mioyo yao imezoea kuwa na tamaa ya mali. Wapo chini ya laana ya Mungu! Wameiacha njia iliyonyoka, wakapotoka na kuifuata njia aliyofuata Balaamu, mwana wa Beori ambaye alipendelea kupata faida kwa kufanya udanganyifu, akakaripiwa kwa ajili ya uovu wake. Punda ambaye hasemi, alinena kwa sauti ya binadamu, akaukomesha wazimu wa huyo nabii. Watu hao ni kama chemchemi zilizokauka, kama mawingu yanayopeperushwa na tufani; makao yao waliyowekewa ni mahali pa giza kuu. Husema maneno ya majivuno na yasiyo na maana, na kutumia tamaa zao mbaya za kimwili kuwatega wale ambao wamejitenga hivi karibuni na watu waishio katika udanganyifu. Huwaahidi watu wengine eti watakuwa huru, kumbe wao wenyewe ni watumwa wa upotovu — maana mtu ni mtumwa wa chochote kile kinachomtawala. Watu waliokwisha ponyoka katika upotovu wa ulimwengu kwa kupata kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, kisha wakakubali kunaswa na kutawaliwa tena na upotovu huo, hali yao itakuwa mbaya zaidi kuliko awali. Ingalikuwa afadhali kwao kama wasingalijua kamwe njia hiyo ya uadilifu kuliko kuijua na kisha kuiacha na kupoteza amri takatifu waliyopokea. Ipo methali isemayo: “Mbwa huyarudia matapishi yake mwenyewe,” na nyingine isemayo: “Nguruwe aliyekwisha oshwa hugaagaa tena katika matope!” Ndivyo ilivyo kwao sasa. Wapenzi wangu, hii ni barua ya pili ninayowaandikia. Katika barua hizo mbili nimejaribu kufufua fikira safi akilini mwenu kwa kuwakumbusheni mambo haya. Napenda mkumbuke maneno yaliyosemwa na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa na mitume wenu. Awali ya yote jueni kwamba siku za mwisho watakuja watu ambao mienendo yao inatawaliwa na tamaa zao mbaya. Watawadhihaki nyinyi na kusema: “Aliahidi kwamba atakuja! Je, sasa yuko wapi? Mambo ni yaleyale tangu babu zetu walipokufa; hali ya vitu ni ileile kama ilivyokuwa mwanzo wa ulimwengu!” Watu hao, kwa makusudi, husahau kwamba zamani Mungu alinena, nazo mbingu na dunia zikaumbwa. Dunia iliumbwa kutoka katika maji na kwa maji; na kwa maji hayo, yaani yale maji ya gharika kuu, dunia ya wakati ule iliangamizwa. Lakini mbingu na dunia ya sasa zahifadhiwa kwa neno la Mungu kwa ajili ya kuharibiwa kwa moto. Zimewekwa kwa ajili ya siku ile ambapo watu wasiomcha Mungu watahukumiwa na kuangamizwa. Lakini, wapenzi wangu, msisahau kitu kimoja! Mbele ya Bwana, hakuna tofauti kati ya siku moja na miaka elfu; kwake yote ni mamoja. Bwana hakawii kutimiza yale aliyoahidi kama watu wengine wanavyofikiri kuwa atakawia. Yeye ana saburi kwa ajili yenu, maana hapendi hata mmoja wenu apotee, bali huwavuta wote wapate kutubu. Siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Siku hiyo, mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; vitu vyake vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia itatoweka pamoja na kila kitu kilichomo ndani yake. Maadamu kila kitu kitaharibiwa namna hiyo, je, nyinyi mnapaswa kuwa watu wa namna gani? Mnapaswa kuishi kitakatifu na kumcha Mungu, mkiingojea siku ile ya Mungu na kuifanya ije upesi — siku ambayo mbingu zitateketezwa kwa moto na kuharibiwa, na vitu vyake vya asili vitayeyushwa kwa joto. Lakini sisi, kufuatana na ahadi yake, twangojea mbingu mpya na dunia mpya ambayo imejaa uadilifu. Kwa hiyo wapenzi wangu, mkiwa mnaingojea siku ile, fanyeni bidii kuwa safi kabisa bila hatia mbele ya Mungu, na kuwa na amani naye. Mnapaswa kuuona uvumilivu wa Bwana kuwa ni nafasi anayowapeni mpate kuokolewa, kama Paulo ndugu yetu mpenzi alivyowaandikia akitumia hekima aliyopewa na Mungu. Hayo ndiyo asemayo katika barua zake zote anapozungumzia suala hilo. Yapo mambo kadhaa katika barua zake yaliyo magumu kuyaelewa, mambo ambayo watu wajinga, wasio na msimamo, huyapotosha kama wanavyopotosha sehemu nyingine za Maandiko Matakatifu. Hivyo wanasababisha maangamizi yao wenyewe. Lakini nyinyi, wapenzi wangu, mmekwisha jua jambo hili. Basi, muwe na tahadhari msije mkapotoshwa na makosa ya waasi, mkaanguka kutoka katika msimamo wenu imara. Lakini endeleeni kukua katika neema na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu uwe kwake, sasa na hata milele! Amina. Habari hii yahusu Neno la uhai lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe. Uhai huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uhai huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu. Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni nyinyi pia, ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo. Tunawaandikia nyinyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike. Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake. Tukisema kwamba tuna umoja naye, na papo hapo tunaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo wala hatuishi kwa ukweli kwa maneno na matendo. Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi, tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe, na ukweli haumo ndani yetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote. Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu. Watoto wangu, ninawaandikieni mambo haya, kusudi msitende dhambi. Lakini, ikijatokea mtu akatenda dhambi, tunaye mmoja ambaye hutuombea kwa Baba, ndiye Yesu Kristo aliye mwadilifu kabisa. Kristo ndiye sadaka iondoayo dhambi zetu; wala si dhambi zetu sisi tu, bali pia dhambi za ulimwengu wote. Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua. Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake. Lakini mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye: Mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo. Wapenzi wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe mliousikia. Hata hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana ndani ya Kristo na ndani yenu pia. Maana giza linatoweka, na mwanga wa kweli umekwisha anza kuangaza. Yeyote asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu huyo bado yumo gizani. Yeyote ampendaye ndugu yake yuko katika mwanga, na hamna chochote ndani yake kiwezacho kumkwaza mtu mwingine. Lakini anayemchukia ndugu yake yumo gizani; anatembea gizani, na hajui anakokwenda, maana giza limempofusha. Ninawaandikieni nyinyi watoto kwa kuwa dhambi zenu zimeondolewa kwa jina la Kristo. Nawaandikieni nyinyi kina baba kwani mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo. Nawaandikieni nyinyi vijana kwa sababu mmemshinda yule Mwovu. Nawaandikieni nyinyi watoto kwa sababu mnamjua Baba. Nawaandikieni nyinyi kina baba kwa kuwa mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo. Nawaandikieni nyinyi vijana kwa sababu mna nguvu; neno la Mungu limo ndani yenu na mumemshinda yule Mwovu. Msiupende ulimwengu, wala chochote kilicho cha ulimwengu. Mtu anayeupenda ulimwengu, upendo wa Baba hauwezi kuwamo ndani yake. Vitu vyote vya ulimwengu — tamaa mbaya za mwili, vitu wanavyoviona watu na kuvitamani, majivuno yasababishwayo na mali — vyote hivyo havitoki kwa Baba, bali vyatoka kwa ulimwengu. Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye atakalo Mungu, anaishi milele. Watoto, mwisho u karibu! Mlikwisha sikia kwamba mpinzani wa Kristo anakuja, na sasa wapinzani wengi wa Kristo wamekwisha fika, na hivyo twajua kwamba mwisho u karibu. Watu hao wametokea kati yetu lakini hawakuwa kweli wa kwetu na ndiyo maana walituacha; kama wangalikuwa wa kwetu, wangalibaki nasi. Lakini waliondoka, wakaenda zao, kusudi ionekane wazi kwamba hawakuwa kamwe wa kwetu. Nyinyi, lakini, mlipata kumiminiwa Roho Mtakatifu na Kristo, na hivyo mnaujua ukweli. Basi, nawaandikieni, si kwa kuwa hamwujui ukweli, bali kwa sababu mnaujua; na pia mnajua kwamba uongo wowote haupatikani katika ukweli. Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Kristo. Mtu wa namna hiyo ni mpinzani wa Kristo — anamkana Baba na Mwana. Maana yeyote anayemkana Mwana, anamkana pia Baba; na yeyote anayemkubali Mwana, anampata Baba pia. Basi, ujumbe ule mliousikia tangu mwanzo na ukae mioyoni mwenu. Kama ujumbe huo mliousikia tangu mwanzo ukikaa ndani yenu, basi, mtaishi daima katika umoja na Mwana na Baba. Na ahadi aliyotuahidia sisi ndiyo hii: Uhai wa milele. Nimewaandikieni mambo haya kuhusu wale wanaotaka kuwapotosha nyinyi. Lakini, kwa upande wenu nyinyi, Kristo aliwatia mafuta kwa Roho wake. Na kama Roho huyo akiendelea kukaa ndani yenu, hamhitaji kufundishwa na mtu yeyote. Maana yeye anawafundisheni kila kitu, na mafundisho yake ni ya kweli, si ya uongo. Basi, shikeni mafundisho ya huyo Roho na kubaki katika muungano na Kristo. Naam, watoto, kaeni ndani yake kusudi wakati atakapotokea tuwe hodari bila kuwa na sababu ya kujificha kwa aibu siku ya kuja kwake. Mnajua kwamba Kristo ni mwadilifu kabisa; basi, mnapaswa kujua pia kwamba kila mtu atendaye mambo adili ni mtoto wa Mungu. Oneni, basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu. Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba, wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo. Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa. Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria. Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna dhambi yoyote. Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona wala kumjua Kristo. Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa. Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi. Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu. Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi. Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa kupendana! Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimuua ndugu yake. Na, kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, lakini yale ya ndugu yake yalikuwa mema! Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia nyinyi. Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uhai kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo. Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule hana uhai wa milele ndani yake. Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu. Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu? Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo. Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu. Kwa maana, hata kama dhamiri zetu zatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu. Wapenzi wangu, kama dhamiri zetu hazina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu, na kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza. Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Yesu Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru. Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi. Wapenzi wangu, msimsadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni. Hii ndiyo njia ya kujua kama mtu anaongozwa na Roho wa Mungu: Kila anayekiri kwamba Kristo alikuja, akawa binadamu, mtu huyo anaye Roho wa Mungu. Lakini mtu yeyote asiyemkiri Kristo hivyo, hana huyo Roho atokaye kwa Mungu. Mtu huyo ana roho ambaye ni wa mpinzani wa Kristo; nanyi mlikwisha sikia kwamba anakuja, na sasa tayari amekwisha wasili ulimwenguni! Lakini nyinyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu. Wao husema mambo ya ulimwengu, nao ulimwengu huwasikiliza kwani wao ni wa ulimwengu. Lakini sisi ni wake Mungu. Mtu anayemjua Mungu hutusikiliza, mtu asiye wa Mungu hatusikilizi. Basi, kwa njia hiyo tunaweza kutambua tofauti kati ya Roho wa ukweli na roho wa uongo. Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu. Kila mtu aliye na upendo ni mtoto wa Mungu, na anamjua Mungu. Mtu asiye na upendo hamjui Mungu, maana Mungu ni upendo. Na Mungu alionesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uhai kwa njia yake. Hivi ndivyo upendo ulivyo: Si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi zetu. Wapenzi wangu, ikiwa Mungu alitupenda hivyo, basi, nasi tunapaswa kupendana. Hakuna mtu aliyekwisha mwona Mungu kamwe; lakini kama tukipendana, Mungu anaishi katika muungano nasi, na upendo wake unakamilika ndani yetu. Tunajua kwamba tunaishi katika umoja na Mungu, naye Mungu anaishi katika umoja nasi, kwani yeye ametupa Roho wake. Sisi tumeona na kuwaambia wengine kwamba Baba alimtuma Mwanae awe Mwokozi wa ulimwengu. Kila mtu anayekiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu anaishi katika muungano na mtu huyo, naye anaishi katika muungano na Mungu. Basi, sisi tunajua na tunaamini upendo alio nao Mungu kwetu sisi. Mungu ni upendo, na kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu, na Mungu anaishi katika muungano naye. Upendo umekamilika ndani yetu kusudi tuweze kuwa na ujasiri siku ile ya hukumu; kwani maisha yetu hapa duniani ni kama yale ya Kristo. Palipo na upendo hapana woga; naam, upendo kamili hufukuza woga wote. Basi, mtu mwenye woga hajakamilika bado katika upendo, kwani woga huhusikana na adhabu. Sisi tuna upendo kwa sababu Mungu alitupenda kwanza. Mtu akisema kwamba anampenda Mungu, hali anamchukia ndugu yake, huyo ni mwongo. Maana mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hamwoni. Basi, hii ndiyo amri aliyotupa Kristo: Anayempenda Mungu anapaswa pia kumpenda ndugu yake. Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ni Kristo, huyo ni mtoto wa Mungu. Kila anayempenda mzazi humpenda pia mtoto wa huyo mzazi. Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu: Kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake; maana kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake. Na, amri zake si ngumu, maana kila aliye mtoto wa Mungu anaweza kuushinda ulimwengu. Hivi ndivyo tunavyoushinda ulimwengu: Kwa imani yetu. Nani, basi, awezaye kuushinda ulimwengu? Ni yule anayeamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. Yesu Kristo ndiye aliyekuja kwa maji ya ubatizo wake na kwa damu ya kifo chake. Hakuja kwa maji tu, bali kwa maji na kwa damu. Naye Roho anashuhudia kwamba ni kweli, kwani Roho ni ukweli. Basi, wako mashahidi watatu: Roho, maji na damu; na ushahidi wa hawa watatu waafikiana. Ikiwa twaukubali ushahidi wa binadamu, ushahidi wa Mungu una uzito zaidi; na huu ndio ushahidi alioutoa Mungu mwenyewe juu ya Mwanae. Anayemwamini Mwana wa Mungu anao ushahidi huo ndani yake; lakini asiyemwamini Mungu, anamfanya yeye kuwa mwongo, maana hakuamini ushahidi alioutoa Mungu juu ya Mwanae. Na, ushahidi wenyewe ndio huu: Mungu alitupatia uhai wa milele, na uhai huo uko kwa Bwana. Yeyote aliye na Mwana wa Mungu anao uhai huo; asiye na Mwana wa Mungu, hana uhai. Nawaandikieni mpate kujua kwamba mnao uhai wa milele nyinyi mnaoamini kwa jina la Mwana wa Mungu. Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya matakwa yake, yeye hutusikiliza. Yeye hutusikiliza kila tunapomwomba; na kwa vile tunajua kwamba yeye hutusikiliza kila tunapomwomba, twajua pia kwamba hutupatia yote tunayomwomba. Mtu akimwona ndugu yake ametenda dhambi isiyompeleka kwenye kifo, anapaswa kumwombea kwa Mungu, naye Mungu atampatia uhai. Nasema jambo hili kuhusu wale waliotenda dhambi ambazo si za kifo. Lakini ipo dhambi yenye kumpeleka mtu kwenye kifo, nami sisemi kwamba mnapaswa kumwomba Mungu kwa ajili ya hiyo. Kila tendo lisilo adilifu ni dhambi, lakini kuna dhambi isiyompeleka mtu kwenye kifo. Tunajua kwamba kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, kwa sababu Mwana wa Mungu humlinda salama, na yule Mwovu hawezi kumdhuru. Tunajua kwamba sisi ni wake Mungu ingawa ulimwengu wote unatawaliwa na yule Mwovu. Twajua pia kwamba Mwana wa Mungu amekuja, akatupa elimu ili tumjue Mungu wa kweli; tuishi katika muungano na Mungu wa kweli — katika muungano na Mwanae, Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na huu ndio uhai wa milele. Watoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu! Mimi mzee nakuandikia wewe Bimkubwa mteule pamoja na watoto wako ninaowapenda kweli. Wala si mimi tu ninayewapenda, bali pia wote wanaoujua ule ukweli wanawapenda nyinyi, kwa sababu ukweli unakaa nasi milele. Neema na huruma na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika ukweli na upendo. Nilifurahi sana kuona kwamba baadhi ya watoto wako wanaishi katika ukweli kama Baba alivyotuamuru. Basi, Bimkubwa, ninalo ombi moja kwako: Tupendane. Ombi hili si amri mpya, bali ni amri ileile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Upendo maana yake ni kuishi kwa kuzitii amri zake Mungu. Amri mliyoisikia tangu mwanzo ndiyo hii: Mnapaswa nyote kuishi katika upendo. Wadanganyifu wengi wamezuka duniani, watu ambao hawakiri kwamba Yesu Kristo amekuja kwetu, na mwili wa kibinadamu. Mtu asemaye hivyo ni mdanganyifu na ni mpinzani wa Kristo. Basi, jihadharini nyinyi wenyewe ili msije mkapoteza kile mlichokishughulikia, bali mpate tuzo lenu kamili. Asiyezingatia na kudumu katika mafundisho ya Kristo, bali anayakiuka, hana Mungu. Lakini anayedumu katika mafundisho hayo anaye Baba na Mwana. Basi, kama mtu akija kwenu bila kuwaleteeni mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani kwenu, wala msimsalimu. Maana anayemsalimu mtu huyo, anashirikiana naye katika matendo yake maovu. Ninayo mengi ya kuwaambieni, lakini sipendi kufanya hivyo kwa karatasi na wino; badala yake, natumaini kuwatembeleeni na kuzungumza nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ikamilike. Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu. Mimi mzee, nakuandikia wewe Gayo, rafiki yangu, ninayekupenda kweli. Mpenzi wangu, nakutakia mafanikio mema ya kila aina; nakutakia afya njema ya mwili kama ulivyo nayo rohoni. Nimefurahi sana ndugu kadhaa walipofika hapa, wakashuhudia juu ya uaminifu wako kuhusu ukweli; naam, wewe unaishi daima katika ukweli. Hakuna kitu kinachonifurahisha zaidi kuliko kusikia kwamba watoto wangu wanaishi katika ukweli. Mpenzi wangu, wewe ni mwaminifu kila mara unapowahudumia ndugu, hata kama ni wageni. Ndugu hao wamelieleza kanisa hapa habari za upendo wako. Tafadhali uwasaidie waendelee na safari yao kwa namna itakayompendeza Mungu. Maana wanaanza safari yao katika utumishi wa Kristo bila kupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasioamini. Basi, sisi tunapaswa kuwasaidia watu hawa, ili nasi tupate kushiriki katika kazi yao kwa ajili ya ukweli. Niliandika barua fupi kwa hilo kanisa; lakini Diotrefe, ambaye hupenda kuwa kiongozi wao, hataki kabisa kunisikiliza. Basi, nitakapokuja nitayafichua mambo yote anayofanya, maneno mabaya anayotutolea na uongo anaosema juu yetu. Isitoshe, yeye hukataa kuwakaribisha hao ndugu walio safarini, na hata huwazuia watu wengine wanaotaka kuwakaribisha, na hujaribu kuwafukuza nje ya kanisa. Mpenzi wangu, usifuate mfano mbaya, bali mfano mwema. Kila atendaye mema ni wa Mungu; lakini anayetenda mabaya hajapata kumwona Mungu. Kila mtu anamsifu Demetrio; naam, ukweli wenyewe unamsifu. Nasi pia tunatoa ushahidi wetu juu yake, nawe wajua kwamba tunachosema ni kweli. Ninayo bado mengi ya kukuambia, lakini sipendi kuyaandika kwa kalamu na wino. Natumaini kukuona karibuni na hapo tutazungumza ana kwa ana. Nakutakia amani. Rafiki zako wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu wote kila mmoja binafsi. Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo na ndugu yake Yakobo, nawaandikia nyinyi mlioitwa na Mungu na ambao mnapendwa naye Mungu Baba, na kuwekwa salama kwa ajili ya Yesu Kristo. Nawatakieni huruma, amani na upendo kwa wingi. Ndugu wapenzi, nilikuwa na mpango wa kuwaandikieni juu ya ule wokovu tunaoshiriki sote, lakini nimeona lazima ya kuwaandikieni nikiwahimizeni mwendelee na juhudi kwa ajili ya imani ambayo Mungu amewajalia watu wake mara moja tu kwa wakati wote. Maana watu wasiomcha Mungu wamepata kujiingiza kwa siri miongoni mwetu, watu ambao, kwa faida ya maisha yao mabaya, wanaupotosha ujumbe wa neema ya Mungu wetu na kumkana Yesu Kristo aliye peke yake Kiongozi na Bwana wetu. Lakini, Maandiko Matakatifu yalikwisha bashiri tangu zamani hukumu inayowangojea watu hao. Sasa nataka kuwakumbusheni mambo fulani, ingawaje haya mlikwisha fahamishwa kikamilifu mara moja: Kumbukeni jinsi Bwana alivyowaokoa watu wa Israeli na kuwatoa katika nchi ya Misri, lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. Na, malaika ambao hawakuridhika na cheo chao, wakayaacha makao yao ya asili, Mungu amewafunga gizani kwa minyororo ya milele wahukumiwe siku ile kuu. Kumbukeni pia Sodoma na Gomora, na miji ya kandokando yake; wenyeji wake walifanya kama wale malaika; walifanya uzinzi na mambo yaliyo kinyume cha maumbile, wakapewa hukumu ya moto wa milele, iwe onyo kwa watu wote. Hivyo ndivyo pia walivyo watu hawa. Ndoto zao huwaongoza katika kuichafua miili yao wenyewe, kuyadharau mamlaka ya Mungu na kuvitukana viumbe vitukufu vya huko juu. Hata Mikaeli, malaika mkuu, hakufanya hivyo. Katika ule ubishi kati yake na Ibilisi juu ya mwili wa Mose, Mikaeli hakuthubutu kumhukumu Ibilisi kwa matusi, ila alisema: “Bwana mwenyewe na akukaripie.” Lakini watu hawa hutukana chochote wasichokielewa; wataangamizwa kwa mambo yaleyale wanayoyajua kwa silika kama wajuavyo wanyama wasio na akili. Ole wao! Watu hao wamefuata mwenendo uleule wa Kaini. Kwa ajili ya fedha, wamejiingiza katika mkosi uleule wa Balaamu. Wameasi kama Kora alivyoasi na wameangamizwa kama yeye alivyoangamizwa. Kwa makelele yao yasiyo na adabu, na kwa kujipendelea wao wenyewe, watu hao ni kama madoa machafu kwenye karamu mnazoshiriki kwa upendo. Wako kama mawingu yasiyo na mvua yanayopeperushwa na upepo. Wao ni kama miti iliyopukutika isiyozaa matunda, iliyokufa kabisa, iliyong'olewa. Watu hao ni kama mawimbi makali ya bahari, na matendo yao ya aibu yanatoka kama povu. Wao ni kama nyota zinazotangatanga ambazo zimewekewa milele mahali pa giza kuu. Naye Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hao: “Sikilizeni! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu kuwahukumu watu wote, na kuwaadhibu wote wasiomcha Mungu kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda bila kumjali Mungu, na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo.” Watu hawa hunung'unika daima, hulalamika, hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kwa faida yao wenyewe. Lakini nyinyi wapenzi wangu, kumbukeni yale mliyoambiwa hapo awali na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Waliwaambieni: “Siku za mwisho, watatokea watu watakaowadhihaki nyinyi, watu wafuatao tamaa zao mbaya.” Hao ndio wanaosababisha mafarakano, watu wa fikira za kidunia, wasio na Roho wa Mungu. Lakini nyinyi, wapenzi wangu, jijengeni wenyewe juu ya imani yenu takatifu kabisa. Salini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, na kudumu katika upendo wa Mungu, mkimngojea Bwana wetu Yesu Kristo ambaye, kwa huruma yake, atawajalieni uhai wa milele. Muwe na huruma kwa watu walio na mashaka; waokoeni kwa kuwanyakua kutoka motoni. Lakini kwa wengine muwe na huruma pamoja na tahadhari, mkichukia hata mavazi yao yenye madoa ya tamaa zao mbaya. Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta nyinyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake, kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina. Huu ni ufunuo aliotoa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa awaoneshe watumishi wake mambo ambayo yanapaswa kutukia karibuni. Kristo alimtuma malaika wake amjulishe mtumishi wake Yohane mambo hayo. Naye Yohane ameshuhudia yote aliyoyaona kuhusu ujumbe wa Mungu na ushahidi wa Yesu Kristo. Heri yake mtu anayesoma kitabu hiki chenye maneno ya ujumbe wa kinabii; na heri yao wanaosikia na kushika yaliyoandikwa humu, maana wakati wa mambo haya umekaribia. Mimi Yohane nayaandikia makanisa saba yaliyoko Asia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi, na kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa kutoka kwa wafu, na ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia. Yeye anatupenda, na kwa damu yake ametufungua kutoka vifungo vya dhambi zetu, akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina. Tazama! Anakuja na mawingu! Kila mtu atamwona, na hata wale waliomtoboa. Makabila yote duniani yataomboleza juu yake. Naam! Amina. “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu Mwenye Nguvu, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja. Mimi ni Yohane, ndugu yenu, ambaye kwa kuungana na Yesu, nashiriki pamoja nanyi mateso na ufalme wake na uvumilivu thabiti. Mimi nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa sababu ya kuhubiri neno la Mungu na kumshuhudia Yesu. Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta. Nayo ilisema, “Andika katika kitabu yale unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamumu, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea.” Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu, na katikati yake kulikuwa na kitu kama Mwana wa Mtu, naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na mkanda wa dhahabu kifuani. Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba nyeupe, kama theluji; macho yake yalimetameta kama moto; miguu yake kama shaba iliyong'arishwa iliyosafishwa katika tanuri ya moto, na sauti yake ilikuwa kama sauti ya poromoko la maji. Katika mkono wake wa kulia alikuwa na nyota saba, na kinywani mwake mlitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake uling'aa kama jua kali kabisa. Basi, nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti. Lakini yeye akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho. Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni hai milele na milele. Ninazo funguo za kifo na kuzimu. Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia sasa na yale yatakayotukia baadaye. Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia na siri ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu, ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa makanisa; na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni makanisa saba. “Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika: “Mimi nishikaye zile nyota saba katika mkono wangu wa kulia na ambaye hutembea katikati ya vinara saba vya taa vya dhahabu, nasema hivi: Najua mambo yako yote; najua bidii yako na uvumilivu wako. Najua kwamba huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewapima wale wanaojisemea kuwa mitume na kumbe sio, ukagundua kwamba ni waongo. Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina langu, wala hukuvunjika moyo. Lakini ninalo jambo moja dhidi yako: Wewe hunipendi tena sasa kama pale awali. Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukatubu na kufanya kama ulivyofanya pale awali. La sivyo, naja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa mahali pake. Lakini nakusifu juu ya kitu kimoja: Wewe unayachukia wanayoyatenda Wanikolai kama ninavyoyachukia mimi. “Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Mshindi nitamjalia kula matunda ya mti wa uhai ulioko ndani ya bustani ya Mungu. “Kwa malaika wa kanisa la Smurna andika: “Mimi niliye wa kwanza na wa mwisho, ambaye nilikufa na kuishi tena, nasema hivi: Najua taabu zako; najua pia umaskini wako, ingawaje kwa kweli wewe ni tajiri; najua kashfa walizokufanyia wale wanaojiita Wayahudi lakini si Wayahudi wa kweli, bali ni kundi lake Shetani. Usiogope hata kidogo yale ambayo itakulazimu kuteseka. Sikiliza! Ibilisi anataka kuwajaribu kwa kuwatia baadhi yenu gerezani; nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Muwe waaminifu hata mpaka kufa, nami nitawapeni taji ya uhai. “Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Mshindi hataumizwa na kifo cha pili. “Kwa malaika wa kanisa la Pergamumu andika: “Mimi niliye na upanga mkali wenye makali kuwili nasema hivi: Najua unakoishi: Wewe unaishi kwenye makao makuu ya Shetani! Lakini bado unashikilia jina langu; hukuikana imani yako kwangu hata siku zile Antipa, shahidi wangu mwaminifu, alipouawa pale mahali anapoishi Shetani. Lakini ninayo machache dhidi yako: Baadhi yenu ni wafuasi wa Balaamu aliyemfundisha Balaki kuwatega wana wa Israeli wale vyakula vilivyotambikiwa sanamu na kufanya uzinzi. Vivyo hivyo, wako pia miongoni mwenu watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai. Basi, tubu. La sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga utokao kinywani mwangu. “Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Mshindi nitampa ile mana iliyofichika. Nitampa pia jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya ambalo hakuna mtu aliyelijua isipokuwa tu wale wanaolipokea. “Kwa malaika wa kanisa la Thuatira andika hivi: “Huu ndio ujumbe wa Mwana wa Mungu, ambaye macho yake yametameta kama moto, na miguu yake inang'aa kama shaba iliyosuguliwa. Najua mambo yako yote. Najua upendo wako, imani yako, utumishi wako na uvumilivu wako. Wewe unafanya vizuri zaidi sasa kuliko pale awali. Lakini nina jambo moja dhidi yako: Wewe unamvumilia yule mwanamke Yezebeli anayejiita nabii, anayefundisha na kuwapotosha watumishi wangu wafanye uzinzi na kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu. Nimempa muda wa kutubu, lakini hataki kuachana na uzinzi wake. Sikiliza! Sasa namtupa kitandani ambapo yeye pamoja na wote waliofanya uzinzi naye watapatwa na mateso makali, kama wasipotubu matendo yao mabaya waliyotenda naye. Tena nitawaua wafuasi wake, ili makanisa yote yatambue kwamba mimi ndiye ninayechunguza mioyo na fikira za watu. “Lakini nyinyi wengine mlioko huko Thuatira ambao hamfuati mafundisho yake Yezebeli na ambao hamkujifunza kile wanachokiita Siri ya Shetani, nawaambieni kwamba sitawapeni mzigo mwingine. Lazima mzingatie yale mliyo nayo sasa mpaka nitakapokuja. “Mshindi na mwenye kuzingatia mpaka mwisho mambo ninayotaka, nitampa mamlaka juu ya watu wa mataifa: Atawaongoza kwa fimbo ya chuma na kuwavunjavunja kama vyombo vya udongo. Mimi pia nimepokea mamlaka hayo kutoka kwa Baba yangu. Tena nitampa nyota ya asubuhi. “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Kwa malaika wa kanisa la Sarde andika: “Mimi niliye na roho saba za Mungu na nyota saba, nasema hivi: Nayajua mambo yako yote; najua unajulikana kuwa na uhai kumbe umekufa! Amka! Imarisha chochote chema kilichokubakia kabla nacho hakijatoweka kabisa. Maana, mpaka sasa, sijayaona matendo yako kuwa ni makamilifu mbele ya Mungu wangu. Kumbuka, basi, yale uliyofundishwa na jinsi ulivyoyasikia, uyatii na kutubu. Usipokesha nitakujia ghafla kama mwizi, na wala hutaijua saa nitakapokujia. Lakini wako wachache huko Sarde ambao hawakuyachafua mavazi yao. Hao wanastahili kutembea pamoja nami wamevaa mavazi meupe. “Mshindi atavikwa hivyo kwa mavazi meupe. Nami sitalifuta jina lake kutoka katika kitabu cha uhai; tena nitamkiri kwamba ni wangu mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika wake. “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Kwa malaika wa kanisa la Filadelfia andika hivi: “Mimi niliye mtakatifu na wa kweli, ambaye nina ule ufunguo wa Daudi na ambaye hufungua na hakuna awezaye kufunga, hufunga na hakuna awezaye kufungua. Nayajua mambo yako yote! Sasa, nimefungua mbele yako mlango ambao hakuna mtu awezaye kuufunga; najua kwamba ingawa huna nguvu sana, hata hivyo, umelitii neno langu wala hukulikana jina langu. Sikiliza! Nitawapeleka kwako watu wa kundi lake Shetani, watu ambao hujisema kuwa ni Wayahudi, kumbe sivyo, ila wanasema uongo. Naam, nitawapeleka kwako na kuwafanya wapige magoti mbele yako, wapate kujua kwamba nimekupenda wewe. Kwa kuwa wewe umezingatia neno langu la kuwa na uvumilivu thabiti, mimi nitakutegemeza salama wakati ule wa dhiki inayoujia ulimwengu mzima, kuwajaribu wote wanaoishi duniani. Naja kwako upesi! Shikilia kwa nguvu ulicho nacho sasa, ili usije ukanyang'anywa na mtu yeyote taji yako. “Mshindi nitamfanya awe nguzo katika hekalu la Mungu wangu, na hatatoka humo kamwe. Pia nitaandika juu yake jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani Yerusalemu mpya, mji ambao utashuka kutoka juu mbinguni kwa Mungu wangu. Tena nitaandika juu yake jina langu jipya. “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Kwa malaika wa kanisa la Laodikea andika hivi: “Mimi niitwaye Amina, shahidi mwaminifu na wa kweli, ambaye ni chanzo cha viumbe vyote alivyoumba Mungu nasema hivi. Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungekuwa kimojawapo: Baridi au moto. Basi, kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si moto, nitakutapika! Wewe unajisema, ‘Mimi ni tajiri; ninajitosheleza, sina haja ya kitu chochote;’ kumbe, hujui kwamba wewe ni mnyonge, unahitaji kuhurumiwa, maskini, kipofu tena uko uchi! Nakushauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto upate kuwa tajiri kweli. Tena afadhali ununue pia vazi jeupe, uvae na kufunika aibu ya uchi wako. Nunua pia mafuta ukapake machoni pako upate kuona. Mimi ndiye mwenye kumwonya na kumrudi yeyote ninayempenda. Kwa hiyo uwe na bidii na kutubu. Sikiliza! Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye, naye atakula pamoja nami. “Mshindi nitamjalia kuketi pamoja nami juu ya kiti changu cha enzi, kama vile mimi mwenyewe nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu juu ya kiti chake cha enzi. “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!” Baada ya hayo nilitazama nikaona mlango umefunguliwa mbinguni. Na ile sauti niliyoisikia pale awali ambayo ilikuwa kama sauti ya tarumbeta, ikasema, “Njoo hapa juu, nami nitakuonesha mambo yatakayotukia baadaye.” Mara nikakumbwa na Roho. Kumbe, huko mbinguni kuna kiti cha enzi na juu yake ameketi mmoja. Huyo aliyeketi juu yake alikuwa kama almasi na jiwe zuri jekundu. Upinde wa mvua ulikuwa unang'aa kama zumaridi na ulikizunguka kiti cha enzi pande zote. Kulikuwa na duara la viti ishirini na vinne kukizunguka kiti cha enzi, na juu ya viti hivyo wazee ishirini na wanne walikuwa wameketi wamevaa mavazi meupe na taji za dhahabu vichwani. Umeme, sauti na ngurumo, vilikuwa vinatoka kwenye hicho kiti cha enzi. Taa saba za moto zilikuwa zinawaka mbele ya hicho kiti cha enzi. Taa hizo ni roho saba za Mungu. Mbele ya kiti cha enzi kulikuwa na kitu kama bahari ya kioo, angavu kama jiwe ling'aalo sana. Katika pande zote za hicho kiti cha enzi na kukizunguka, kulikuwa na viumbe hai wanne. Viumbe hao walikuwa wamejaa macho mbele na nyuma. Kiumbe wa kwanza alikuwa kama simba, wa pili kama ng'ombe, wa tatu alikuwa na sura ya mtu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka. Viumbe hao wanne walikuwa na mabawa sita kila mmoja, na walikuwa wamejaa macho, ndani na nje. Usiku na mchana, bila kupumzika, huimba: “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu, Bwana, Mungu Mwenye Nguvu, aliyekuwako, aliyeko na anayekuja!” Kila mara viumbe hao wanne walipomtukuza na kumheshimu na kumshukuru huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi ambaye anaishi milele na milele, wale wazee ishirini na wanne hujiangusha mbele ya huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi na kumwabudu huyo ambaye anaishi milele na milele; na huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi wakisema: “Wastahili ee Bwana na Mungu wetu, kupokea utukufu na heshima na nguvu. Maana wewe uliumba vitu vyote, na kwa matakwa yako viliumbwa na vipo.” Kisha nikaona kitabu katika mkono wa kulia wa huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, nacho kilikuwa kimeandikwa ndani na nje na kufungwa kwa mihuri saba. Tena nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kubwa: “Nani anayestahili kuvunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu hicho?” Lakini hakupatikana mtu yeyote mbinguni, wala duniani, wala chini kuzimu, aliyeweza kukifungua hicho kitabu au kukitazama ndani. Basi, mimi nikalia sana kwa sababu hakupatikana mtu aliyestahili kukifungua, au kukitazama ndani. Kisha mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda, chipukizi wa Daudi, ameshinda. Yeye anaweza kuivunja mihuri yake saba na kukifungua hicho kitabu.” Kisha nikaona pale katikati ya kiti cha enzi Mwanakondoo amesimama, akizungukwa kila upande na wale viumbe hai wanne, na wale wazee. Huyo Mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba ambayo ni roho saba za Mungu zilizokuwa zimepelekwa kila mahali duniani. Mwanakondoo akaenda, akakitwaa hicho kitabu kutoka mkono wa kulia wa yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi. Mara tu alipokwisha twaa hicho kitabu, wale viumbe hai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne walianguka kifudifudi mbele ya Mwanakondoo. Kila mmoja alikuwa na kinubi na bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni sala za watu wa Mungu. Basi, wakaimba wimbo huu mpya: “Wewe wastahili kukitwaa hicho kitabu na kuivunja mihuri yake. Kwa sababu wewe umechinjwa, na kwa damu yako umemnunulia Mungu wetu watu kutoka kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Umewafanya ufalme wa makuhani wamtumikie Mungu wetu, nao watatawala duniani.” Kisha nikatazama, nikasikia sauti ya malaika wengi sana, idadi isiyohesabika, maelfu na maelfu. Walikuwa wamekaa kuzunguka kiti cha enzi, wale viumbe hai wanne na wale wazee; wakasema kwa sauti kuu: “Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, utukufu na sifa.” Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini ya dunia na baharini — viumbe vyote ulimwenguni — vikisema: “Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo, iwe sifa na heshima na utukufu na enzi, milele na milele.” Na wale viumbe hai wanne wakasema, “Amina!” Na wale wazee wakaanguka kifudifudi, wakaabudu. Kisha, nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa ile mihuri saba. Nikasikia mmoja wa wale viumbe hai wanne akisema kwa sauti kama ya ngurumo, “Njoo!” Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe hapo. Na mpandafarasi wake alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka kama mshindi, aendelee kushinda. Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe hai wa pili akisema, “Njoo!” Nami nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo, mwekundu. Mpandafarasi wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani duniani, watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa. Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe hai wa tatu akisema, “Njoo!” Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mmoja hapo, mweusi. Mpandafarasi wake alikuwa na vipimo viwili vya kupimia uzito mkononi mwake. Nikasikia kitu kama sauti itokayo kwa wale viumbe hai wanne. Nayo ilisema, “Kibaba kimoja cha unga wa ngano kwa kiasi cha fedha denari moja, na vibaba vitatu vya shayiri kwa denari moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!” Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa nne. Nikamsikia yule kiumbe hai wa nne akisema, “Njoo!” Nami nikatazama, na kumbe alikuwapo farasi mmoja hapo, rangi yake kijivu. Na jina la mpandafarasi wake lilikuwa Kifo, na Kuzimu alimfuata nyuma. Hao walipewa mamlaka juu ya robo moja ya dunia, wawaue watu kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia. Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa tano. Nikaona pale chini ya madhabahu ya kufukizia ubani roho za wale waliouawa kwa sababu ya ujumbe wa Mungu, na kwa sababu ya ushuhuda waliotoa. Basi, wakalia kwa sauti kubwa: “Ee Bwana, uliye mtakatifu na mwaminifu, mpaka lini utakawia kulipiza kisasi kwa wakazi wote wa dunia kwa ajili ya kuuawa kwetu?” Wakapewa kila mmoja vazi refu jeupe, wakaambiwa wazidi kusubiri kwa muda mfupi, mpaka itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu ambao watauawa kama wao wenyewe walivyouawa. Kisha nikatazama, na wakati Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa sita, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi; jua likawa jeusi kama gunia la manyoya; mwezi wote ukawa mwekundu kama damu; nazo nyota za mbingu zikaanguka juu ya ardhi kama matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. Anga likatoweka kama vile karatasi inavyokunjwakunjwa; milima yote na visima vyote vikaondolewa mahali pake. Kisha, wafalme wa duniani, wakuu, majemadari, matajiri, wenye nguvu, kila mtumwa na mtu huru, wakajificha mapangoni na kwenye miamba milimani. Wakaiambia hiyo milima na hayo majabali, “Tuangukieni, mkatufiche mbali na yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na mbali na ghadhabu ya Mwanakondoo! Maana siku maalumu ya ghadhabu yao imefika. Nani awezaye kuikabili?” Baada ya hayo nikawaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za dunia, wakishika pepo nne za dunia ili upepo usivume hata kidogo: Wala katika nchi, wala baharini, wala kwenye miti. Kisha, nikamwona malaika mwingine akipanda juu kutoka mashariki, akiwa na mhuri wa Mungu aliye hai. Akapaza sauti na kuwaambia hao malaika wanne waliokabidhiwa jukumu la kuiharibu nchi na bahari, “Msiharibu nchi, wala bahari, wala miti, mpaka tutakapokwisha wapiga mhuri watumishi wa Mungu wetu katika paji la uso.” Kisha, nikasikia idadi ya hao waliopigwa mhuri: Watu 144,000 wa makabila yote ya watu wa Israeli. Kabila la Yuda, watu 12,000; kabila la Reubeni, 12,000; kabila la Gadi, 12,000; kabila la Asheri, 12,000; kabila la Naftali, 12,000; kabila la Manase, 12,000; kabila la Simeoni, 12,000; kabila la Lawi, 12,000; kabila la Isakari, 12,000; kabila la Zebuluni, 12,000; kabila la Yosefu, 12,000; na kabila la Benyamini, 12,000. Kisha, nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu wasiohesabika: Watu wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha. Nao walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wamevaa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao. Wakapaza sauti: “Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwanakondoo!” Malaika wote wakasimama kukizunguka kiti cha enzi, wazee na wale viumbe hai wanne. Wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu, wakisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!” Mmoja wa hao wazee akaniuliza, “Hawa waliovaa mavazi meupe ni watu gani? Na wametoka wapi?” Nami nikamjibu, “Mheshimiwa, wewe wajua!” Naye akaniambia, “Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, yakawa meupe kabisa. Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia Mungu mchana na usiku katika hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda. Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena, kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uhai. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.” Na Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa saba, kukawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa. Kisha, nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele ya Mungu wamepewa tarumbeta saba. Malaika mwingine akafika, anachukua chetezo cha dhahabu, akasimama mbele ya madhabahu ya kufukizia ubani. Naye akapewa ubani mwingi autoe sadaka pamoja na sala za watu wote wa Mungu juu ya madhabahu ya dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi. Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa Mungu kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu. Kisha, malaika akakichukua hicho chetezo, akakijaza moto wa madhabahuni, akakitupa duniani. Kukawa na ngurumo, sauti, umeme na tetemeko la ardhi. Kisha, wale malaika saba wenye tarumbeta saba wakajiweka tayari kupiga mbiu ya mgambo. Malaika wa kwanza akapiga tarumbeta yake. Mchanganyiko wa mvua ya mawe na moto pamoja na damu ukamwagwa juu ya nchi. Theluthi moja ya nchi ikaungua, theluthi moja ya miti ikaungua na majani yote mabichi yakaungua. Kisha malaika wa pili akapiga tarumbeta yake. Na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi moja ya bahari ikawa damu, theluthi moja ya viumbe vya baharini vikafa, na theluthi moja ya meli zikaharibiwa. Kisha, malaika wa tatu akapiga tarumbeta yake. Na nyota kubwa ikiwaka kama bonge la moto ikaanguka kutoka mbinguni na kutua juu ya theluthi moja ya mito na chemchemi za maji. (Nyota hiyo inaitwa “Uchungu.”) Basi, theluthi moja ya maji yakawa machungu; watu wengi wakafa kutokana na maji hayo, kwa sababu yaligeuka kuwa machungu. Kisha, malaika wa nne akapiga tarumbeta yake. Ndipo theluthi moja ya jua, ya mwezi na ya nyota ikapata pigo; hata mwangaza ukapoteza theluthi moja ya mng'ao wake. Theluthi moja ya mchana ikakosa mwanga, hali kadhalika na theluthi moja ya usiku. Kisha, nikatazama, nikasikia tai akiruka juu kabisa angani, anasema kwa sauti kubwa, “Ole, ole, ole kwa wanaoishi duniani wakati malaika watatu waliobaki watakapopiga tarumbeta zao!” Kisha, malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa ufunguo wa shimo la kuzimu. Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la kuzimu, kukatoka moshi wa tanuri kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa kuzimu. Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani, wakapewa nguvu kama ya nge. Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la uso. Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu wakati anapoumwa na nge. Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia. Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu. Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba. Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi wanaokimbilia vitani. Walikuwa na mikia na miiba kama nge, na kwa mikia hiyo, walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano. Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani Mwangamizi. Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata. Kisha, malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya Mungu. Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Eufrate!” Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo wa mwaka huohuo, kuua theluthi moja ya wanadamu. Nilisikia idadi ya majeshi wapandafarasi ilikuwa 200,000,000. Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapandafarasi katika hiyo njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi ya samawati na manjano kama madini ya kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya simba; na moto, moshi, na madini ya kiberiti vilikuwa vinatoka vinywani mwao. Theluthi moja ya wanadamu waliuawa kwa mabaa hayo matatu, yaani moto, moshi na madini ya kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao; maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na katika mikia yao. Mikia yao ilifanana na nyoka na ilikuwa na vichwa, nao waliitumia hiyo kuwadhuru watu. Wanadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa hayo, hawakutubu na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao wenyewe; wala kuacha kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea. Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi, uzinzi, na wizi. Kisha, nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto. Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na wa kushoto juu ya nchi kavu, na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo. Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: “Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri; usiyaandike!” Kisha, yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni, akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo. Akasema, “Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha! Lakini wakati yule malaika wa saba atakapotoa sauti ya tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama alivyowatangazia watumishi wake manabii.” Kisha, ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni pale awali ikasema nami tena: “Nenda ukakichukue kile kitabu kilichofunguliwa, kilicho mkononi mwa malaika asimamaye juu ya bahari na juu ya nchi kavu.” Basi, nikamwendea huyo malaika, nikamwambia anipe hicho kitabu kidogo. Naye akaniambia, “Kichukue, ukile. Kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali, lakini tumboni kitakuwa kichungu!” Basi, nikakichukua kitabu hicho kidogo kutoka mkononi mwa huyo malaika, nikakila. Nacho kilikuwa kitamu kinywani mwangu kama asali, lakini nilipokimeza kikawa kichungu tumboni mwangu. Kisha, nikaambiwa, “Inakubidi tena kutoa unabii kuhusu watu wengi, mataifa, watu wa lugha nyingi na wafalme!” Kisha nikapewa mwanzi uliokuwa kama kijiti cha kupimia, nikaambiwa, “Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, madhabahu ya kufukizia ubani na kawahesabu watu wanaoabudu ndani ya hekalu. Lakini uache ukumbi ulio nje ya hekalu; usiupime, maana huo umekabidhiwa watu wa mataifa mengine, ambao wataukanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arubaini na miwili. Nami nitawatuma mashahidi wangu wawili ili watoe unabii kwa muda huo wa siku 1,260, wakiwa wamevaa mavazi ya gunia.” Hao mashahidi wawili ni miti miwili ya mizeituni na taa mbili zinazosimama mbele ya Bwana wa dunia. Kama mtu akijaribu kuwadhuru, moto hutoka kinywani mwao na kuwaangamiza maadui zao; na kila mtu atakayejaribu kuwadhuru atakufa namna hiyo. Hao wanayo mamlaka ya kufunga anga, mvua isinyeshe wakati wanapotoa unabii. Tena wanayo mamlaka ya kuzigeuza chemchemi zote za maji ziwe damu, na ya kusababisha maafa ya kila namna duniani kila mara wanapopenda. Lakini wakisha maliza kutoa unabii huo, mnyama atokaye shimoni kuzimu atapigana nao, atawashinda na kuwaua. Maiti zao zitabaki katika barabara za mji mkuu ambapo Bwana wao alisulubiwa. Jina la kupanga la mji huo ni Sodoma au Misri. Watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti hizo kwa muda wa siku tatu na nusu, na hawataruhusu zizikwe. Watu waishio duniani watafurahia kifo cha hao wawili. Watafanya sherehe na kupelekeana zawadi, maana manabii hawa wawili walikuwa wamewasumbua mno watu wa dunia. Lakini baada ya zile siku tatu na nusu pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu. Kisha, hao manabii wawili wakasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njoni hapa juu!” Nao wakapanda juu mbinguni katika wingu, maadui zao wakiwa wanawatazama. Wakati huohuo, kukatokea tetemeko kubwa la ardhi, sehemu moja ya kumi ya ardhi ikaharibiwa. Watu 7,000 wakauawa kwa tetemeko hilo la ardhi. Watu waliosalia wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni. Maafa ya pili yamepita; lakini tazama! Maafa ya tatu yanafuata hima. Kisha, malaika wa saba akapiga tarumbeta yake. Na sauti kuu zikasikika mbinguni zikisema, “Sasa ufalme wa ulimwengu ni wa Bwana wetu na Kristo wake. Naye atatawala milele na milele!” Kisha, wale wazee ishirini na wanne walioketi mbele ya Mungu katika viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, wakisema: “Tunakushukuru ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu, uliyeko na uliyekuwako! Maana umetumia nguvu yako kuu, ukaanza kutawala! Watu wa mataifa waliwaka hasira, lakini ghadhabu yako imefika, naam wakati wa kuwahukumu wafu. Ndio wakati wa kuwatuza watumishi wako manabii, watakatifu na wote wanaolitukuza jina lako, wakubwa kwa wadogo. Ni wakati wa kuwaangamiza waangamizi wa dunia.” Kisha hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana hekaluni mwake. Kukatokea umeme, sauti, ngurumo, tetemeko la ardhi, na mvua kubwa ya mawe. Kisha, ishara kubwa ikaonekana mbinguni: Mwanamke aliyevikwa jua na mwezi chini ya miguu yake na taji ya nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake! Alikuwa mjamzito, naye akapaza sauti kwa maumivu na uchungu wa kujifungua mtoto. Kisha, ishara nyingine ikatokea mbinguni: Joka kubwa jekundu na lenye pembe kumi na vichwa saba; na kila kichwa kilikuwa na taji. Joka hilo liliburuta kwa mkia wake theluthi moja ya nyota za anga na kuzitupa duniani. Nalo lilisimama mbele ya huyo mama aliyekuwa karibu kujifungua mtoto, tayari kabisa kummeza mtoto, mara tu atakapozaliwa. Kisha, mama huyo akajifungua mtoto wa kiume ambaye atayatawala mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Lakini mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu na kwenye kiti chake cha enzi. Huyo mama akakimbilia jangwani ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali pa usalama ambapo angehifadhiwa kwa muda wa siku 1,260. Kisha, kukazuka vita mbinguni: Mikaeli na malaika wake walipigana na hilo joka, nalo likawashambulia pamoja na malaika wake. Lakini joka hilo na malaika wake walishindwa, na hatimaye hapakuwa tena na nafasi mbinguni kwa ajili yao. Basi, joka hilo kuu likatupwa nje. Joka hilo ndiye yule nyoka wa kale ambaye huitwa pia Ibilisi au Shetani ambaye huudanganya ulimwengu wote. Naam, alitupwa duniani, na malaika wake wote pamoja naye. Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikisema: “Sasa umefika ukombozi na nguvu na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake! Maana yule aliyewashtaki ndugu zetu mbele ya Mungu ametupwa chini. Naam, ametupwa chini huyo anayewashtaki usiku na mchana. Ndugu zetu wamemshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno waliloshuhudia; maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana, wakawa tayari kufa. Kwa sababu hiyo, furahini enyi mbingu na vyote vilivyomo ndani yenu. Lakini, ole wenu nchi na bahari, maana Ibilisi amewajieni akiwa na ghadhabu kuu, kwa sababu anajua kwamba muda wake uliobakia ni mfupi.” Joka lilipotambua kwamba limetupwa chini duniani, likaanza kumwinda yule mama aliyekuwa amejifungua mtoto wa kiume. Lakini mama huyo akapewa mabawa mawili ya tai apate kuruka mbali sana na hilo joka, mpaka mahali pake jangwani ambapo angehifadhiwa salama kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Basi, joka likatapika maji mengi kama mto, yakamfuata huyo mama nyuma ili yamchukue. Lakini nchi ikamsaidia huyo mama: Ikajifunua kama mdomo na kuyameza maji hayo yaliyotoka kinywani mwa hilo joka. Basi, joka hilo likamkasirikia huyo mama, likajiondokea, likaenda kupigana na wazawa wengine wa huyo mama, yaani wote wanaotii amri za Mungu na kumshuhudia Yesu. Basi, likajisimamia ukingoni mwa bahari. Kisha nikaona mnyama mmoja akitoka baharini. Alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na kila pembe ilikuwa na taji. Jina la kashfa lilikuwa limeandikwa juu ya vichwa hivyo. Mnyama huyo niliyemwona alikuwa kama chui; miguu yake kama ya dubu na kinywa chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama nguvu yake, kiti chake cha enzi na uwezo mkuu. Kichwa kimojawapo cha huyo mnyama kilionekana kama kilikwisha jeruhiwa vibaya sana, lakini jeraha hilo lilikuwa limepona. Dunia nzima ilishangazwa na huyo mnyama na kumfuata. Watu wote wakaliabudu lile joka kwa sababu lilimpa huyo mnyama uwezo wake. Wakamwabudu pia huyo mnyama wakisema, “Nani aliye kama huyu mnyama? Ni nani awezaye kupigana naye?” Kisha huyo mnyama akaruhusiwa kusema maneno ya kujigamba na kumkufuru Mungu; akaruhusiwa kuwa na mamlaka kwa muda wa miezi arubaini na miwili. Basi, akaanza kumtukana Mungu, kulitukana jina lake, makao yake, na wote wakaao mbinguni. Aliruhusiwa kuwapiga vita na kuwashinda watu wa Mungu. Alipewa mamlaka juu ya watu wa kila kabila, ukoo, lugha na taifa. Wote waishio duniani watamwabudu isipokuwa tu wale ambao majina yao yameandikwa tangu mwanzo wa ulimwengu katika kitabu cha uhai cha Mwanakondoo aliyechinjwa. Aliye na masikio, na asikie! Aliyepangiwa kuchukuliwa mateka lazima atatekwa; wa kuuawa kwa upanga atauawa kwa upanga. Hivyo, watu wa Mungu na wawe na uvumilivu na imani. Kisha, nikamwona mnyama mwingine anatoka ardhini. Alikuwa na pembe mbili kama pembe za kondoo, na aliongea kama joka. Alikuwa na mamlaka kamili kutoka kwa yule mnyama wa kwanza, na akautumia uwezo huo mbele ya huyo mnyama. Akailazimisha dunia yote na wote waliomo humo kumwabudu huyo mnyama wa kwanza ambaye alikuwa na jeraha la kifo lililokuwa limepona. Basi, huyu mnyama wa pili akafanya miujiza mikubwa hata akasababisha moto kutoka mbinguni ushuke duniani mbele ya watu. Aliwapotosha wakazi wa dunia kwa miujiza hiyo aliyojaliwa kutenda mbele ya mnyama wa kwanza. Aliwaambia wakazi wa dunia watengeneze sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi tena. Kisha alijaliwa kuipulizia uhai hiyo sanamu ya yule mnyama wa kwanza, hata ikaweza kuongea na kuwaua watu wote ambao hawakuiabudu. Aliwalazimisha wote, wadogo na wakubwa, matajiri na maskini, watu huru na watumwa, watiwe alama juu ya mikono yao ya kulia au juu ya paji za nyuso zao. Akapiga marufuku mtu yeyote kununua au kuuza kitu isipokuwa tu mtu aliyetiwa alama hiyo, yaani jina la yule mnyama au tarakimu ya jina hilo. Hapa panatakiwa hekima! Mwenye akili anaweza kufafanua maana ya tarakimu ya mnyama huyo, maana ni tarakimu yenye maana ya mtu fulani. Tarakimu hiyo ni 666. Kisha, nikaona mlima Siyoni na Mwanakondoo amesimama juu yake; pamoja naye walikuwa watu 144,000 ambao juu ya paji za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la Baba yake. Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa kama ya maji mengi na kama ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia ilikuwa kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao. Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu 144,000 waliokombolewa duniani. Watu hao ndio wale ambao hawakujichafua na wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako. Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwanakondoo. Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote. Kisha, nikamwona malaika mwingine anaruka juu angani akiwa na Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu waishio duniani, kwa mataifa yote, makabila yote na watu wa lugha zote na rangi zote. Naye akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumtukuza! Maana saa imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na dunia, bahari na chemchemi za maji.” Malaika wa pili alimfuata huyo wa kwanza akisema, “Ameanguka! Naam, Babuloni mkuu ameanguka! Babuloni ambaye aliwapa mataifa yote wainywe divai yake — divai kali ya uzinzi wake!” Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake, yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji. Mtu huyo atateseka ndani ya moto wa madini ya kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwanakondoo. Moshi wa moto unaowatesa hupanda juu milele na milele. Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa alama ya jina lake, hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana.” Hivyo, ni lazima watu wa Mungu, yaani wale wanaotii amri za Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu. Kisha, nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika! Heri watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana.” Naye Roho asema, “Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao yatawafuata.” Kisha, nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo alikuwako aliye kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkali mkononi mwake. Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, na kwa sauti kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, “Tafadhali, tumia mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia yameiva.” Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa. Kisha, malaika mwingine akatoka katika hekalu mbinguni akiwa na mundu wenye makali. Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni, akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali, “Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva!” Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo cha ghadhabu ya Mungu. Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya mji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko wenye kina kufikia hatamu za farasi na urefu upatao kilomita 300. Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya kushangaza. Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa saba ya mwisho. Kwa mabaa hayo saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa. Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na moto. Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na ambaye jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa wamesimama kando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na Mungu. Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu na wa Mwanakondoo: “Bwana Mungu Mwenye Nguvu, matendo yako ni makuu na ya ajabu mno! Ewe Mfalme wa mataifa, njia zako ni za haki na za kweli! Bwana, ni nani asiyekucha wewe? Nani asiyelitukuza jina lako? Wewe peke yako ni Mtakatifu. Mataifa yote yatakujia na kukuabudu maana matendo yako ya haki yamedhihirishwa.” Baada ya hayo nikaona hekalu limefunguliwa mbinguni, na ndani yake hema ya kuwapo kwa Mungu. Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo hekaluni, wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung'aa na kanda za dhahabu vifuani mwao. Kisha, mmojawapo wa wale viumbe wanne akawapa hao malaika saba mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu ya Mungu, na hakuna mtu aliyeweza kuingia hekaluni mpaka mwisho wa mabaa saba ya wale malaika saba. Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu duniani.” Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu ya nchi. Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na alama ya yule mnyama na wale walioiabudu sanamu yake. Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo bahari ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini vikafa. Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, navyo vikageuka damu. Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema, “Ewe mtakatifu, uliyeko na uliyekuwako! Wewe umetenda sawa kuhukumu mambo hayo. Maana waliimwaga damu ya watu wa Mungu na manabii, nawe umewapa damu wainywe; wamestahili hivyo!” Kisha, nikasikia sauti madhabahuni ikisema, “Naam, Bwana Mungu Mwenye Nguvu! Hukumu zako ni za kweli na haki!” Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua likapewa nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake. Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu aliye na uwezo juu ya mabaa hayo. Lakini hawakutubu na kumtukuza Mungu. Kisha, malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao makuu ya yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu, wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na madonda yao. Lakini hawakutubu matendo yao mabaya. Kisha, malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ikawekwa kwa ajili ya wafalme kutoka mashariki. Kisha, nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura, wakitoka kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama na kinywani mwa yule nabii wa uongo. Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio wanaokwenda kwa wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya vita ya ile siku kubwa ya Mungu Mwenye Nguvu. “Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye na kuvaa nguo zake ili asije akaenda uchi huko na huko na kuaibika hadharani.” Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo kwa Kiebrania Harmagedoni. Kisha, malaika wa saba akamwaga bakuli lake hewani. Sauti kubwa ikasikika kutoka kwenye kiti cha enzi, hekaluni, ikisema, “Imetendeka!” Kukatokea umeme, kelele, ngurumo na tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijapata kutokea tangu Mungu alipomuumba mtu. Mji ule mkuu ukapasuliwa sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikateketea. Babuloni, mji mkuu, haukusahauliwa na Mungu. Aliunywesha kikombe cha divai ya ghadhabu ya hasira yake. Visiwa vyote vikatoweka, nayo milima haikuonekena tena. Mvua ya mawe makubwa yenye uzito wa kama kilo hamsini kila moja, ikawanyeshea watu. Nao wakamtukana Mungu kwa sababu ya mapigo ya mvua hiyo ya mawe. Naam, pigo la mvua hiyo ya mawe lilikuwa kubwa mno. Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja, akaniambia, “Njoo, nami nitakuonesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu, mji ule uliojengwa juu ya maji mengi. Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi wa dunia wamelewa divai ya uzinzi wake.” Kisha, nikakumbwa na Roho mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa ameandikwa kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu. Mkononi mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na mambo machafu yanayoonesha uzinzi wake. Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo “Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana duniani.” Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu. Nilipomwona nilishangaa mno. Lakini malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Mimi nitakuambia maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye ambaye ana vichwa saba na pembe kumi. Huyo mnyama uliyemwona, alikuwa hai hapo awali lakini sasa amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao majina yao hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uhai tangu mwanzo wa ulimwengu, watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali aliishi, kisha akafa na sasa anatokea tena! “Hapa panahitaji akili na hekima! Hivyo vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke anaketi juu yake. Vichwa hivyo pia ni wafalme saba. Kati ya hao wafalme saba, watano wamekwisha angamia, mmoja anatawala bado na yule mwingine bado hajafika; na atakapofika atabaki kwa muda mfupi. Huyo mnyama ambaye alikuwa anaishi hapo awali lakini sasa haishi tena ni mfalme wa nane, naye pia ni miongoni mwa hao saba, na anakwenda zake kuharibiwa. “Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme ambao bado hawajaanza kutawala. Lakini watapewa mamlaka ya kutawala kwa muda wa saa moja pamoja na yule mnyama. Shabaha ya hawa kumi ni moja, na watampa yule mnyama nguvu na mamlaka yao yote. Watapigana na Mwanakondoo, lakini Mwanakondoo pamoja na wale aliowaita na kuwachagua ambao ni waaminifu, atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme.” Malaika akaniambia pia, “Yale maji uliyoyaona pale alipokaa yule mzinzi: Ni makundi ya watu wa kila taifa, rangi na lugha. Pembe zile kumi ulizoziona na yule mnyama watamchukia huyo mzinzi. Watachukua kila kitu alicho nacho na kumwacha uchi; watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto. Maana Mungu ametia mioyoni mwao nia ya kutekeleza shabaha yake, yaani wakubaliane wao kwa wao na kumpa huyo mnyama mamlaka yao ya kutawala, mpaka hapo yale aliyosema Mungu yatakapotimia. “Na yule mwanamke uliyemwona ndio ule mji mkuu ulio na mamlaka juu ya wafalme wa dunia.” Baada ya hayo, nilimwona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa na uwezo mkuu, na dunia ikamulikwa na mng'ao wake. Basi, akapaza sauti kwa nguvu akisema, “Umeanguka; Babuloni mkuu umeanguka! Sasa umekuwa makao ya mashetani na pepo wachafu; umekuwa makao ya ndege wachafu na wa kuchukiza mno. Maana mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na anasa zake zisizo na kipimo.” Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema, “Watu wangu, ondokeni kwake, ili msishirikiane naye katika dhambi zake, msije mkaipata adhabu yake. Kwa maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno, zimerundikana mpaka mbinguni, na Mungu ameyakumbuka maovu yake. Mtendeeni kama alivyowatendea nyinyi; mlipeni mara mbili kwa yale aliyoyatenda. Mchanganyieni kikombeni mwake kinywaji kikali maradufu. Mpeni mateso na uchungu kadiri ya kujigamba kwake, kulingana na kuishi kwake kwa anasa. Maana anajisemea moyoni: ‘Ninaketi hapa; mimi ni malkia. Mimi si mjane, wala sitapatwa na uchungu!’ Kwa sababu hiyo mabaa yake yatampata kwa siku moja: Ugonjwa, huzuni na njaa. Atachomwa moto, maana Bwana Mungu mwenye kumhukumu ana nguvu.” Wafalme wa dunia waliofanya uzinzi naye na kuishi naye maisha ya anasa wataomboleza na kulia wakati watakapoona moshi wa mji huo unaoteketea. Wanasimama kwa mbali kwa sababu ya kuogopa mateso yake na kusema, “Ole! Ole kwako Babuloni, mji maarufu na wenye nguvu! Kwa muda wa saa moja tu adhabu yako imekupata.” Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumfanyia matanga, maana hakuna mtu anayenunua tena bidhaa zao; hakuna tena wa kununua dhahabu yao, fedha, mawe ya thamani na lulu, kitani na nguo za rangi ya zambarau, hariri na nguo nyekundu; vyombo vya kila aina ya miti ya pekee, vyombo vya pembe za ndovu, vya miti ya thamani kubwa, vya shaba, chuma na marumaru; mdalasini, viungo, ubani, manemane, udi, divai, mafuta, unga na ngano, ng'ombe na kondoo, farasi na magari ya kukokotwa, watumwa wao na hata maisha ya watu. Wafanyabiashara wanamwambia: “Faida yote uliyotazamia imetoweka, na utajiri na fahari vimekuponyoka; hutaweza kuvipata tena!” Wafanyabiashara waliotajirika kutokana na mji huo, watasimama mbali kwa sababu ya hofu ya mateso yake, watalalamika na kuomboleza, wakisema, “Ole! Ole kwa mji huu mkuu. Ulizoea kuvalia nguo za kitani, za rangi ya zambarau na nyekundu, na kujipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu! Kwa saa moja tu utajiri wako umetoweka!” Halafu manahodha wote na wasafiri wao, wanamaji na wote wanaofanya kazi baharini, walisimama kwa mbali, na walipouona moshi wa moto ule uliouteketeza, wakalia kwa sauti: “Hakujapata kuwako mji kama mji huu mkuu!” Wakajimwagia vumbi juu ya vichwa vyao wakilia kwa sauti na kuomboleza: “Ole! Ole kwako mji mkuu! Ni mji ambamo wote wenye meli zisafirizo baharini walitajirika kutokana na utajiri wake. Kwa muda wa saa moja tu umepoteza kila kitu! “Furahi ee mbingu, kwa sababu ya uharibifu wake. Furahini watu wa Mungu, mitume na manabii! Kwa maana Mungu ameuhukumu kwa sababu ya mambo uliyowatenda nyinyi!” Kisha, malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe mfano wa jiwe kubwa la kusagia, akalitupa baharini akisema, “Ndivyo Babuloni atakavyotupwa na kupotea kabisa. Sauti za vinubi za muziki, sauti za wapiga filimbi na tarumbeta hazitasikika tena ndani yako. Hakuna fundi wa namna yoyote ile atakayepatikana tena ndani yako; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikika tena ndani yako. Mwanga wa taa hautaonekana tena ndani yako; sauti za bwana arusi na bibi arusi hazitasikika tena ndani yako. Wafanyabiashara wako walikuwa wakuu duniani, na kwa uchawi wako mataifa yote yalipotoshwa!” Mji huo uliadhibiwa kwani humo mlipatikana damu ya manabii, damu ya watakatifu na ya watu wote waliouawa duniani. Baada ya hayo nikasikia kitu kama sauti kubwa ya umati wa watu wengi mbinguni ikisema, “Asifiwe Mungu! Ukombozi, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu! Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki. Amemhukumu yule mzinzi mkuu ambaye alikuwa ameipotosha dunia kwa uzinzi wake. Amemwadhibu kwa sababu ya kumwaga damu ya watumishi wake!” Wakasema, “Asifiwe Mungu! Moshi wa moto unaoteketeza mji huo utapanda juu milele na milele!” Na wale wazee ishirini na wanne, na wale viumbe hai wanne, wakajitupa chini, wakamwabudu Mungu aliyeketi juu ya kiti cha enzi wakisema, “Amina! Asifiwe Mungu!” Kisha, kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: “Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.” Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, “Asifiwe Mungu! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Nguvu ametawala! Tufurahi na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa harusi ya Mwanakondoo umefika, na bibi arusi yuko tayari. Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung'aa!” (Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watakatifu). Kisha malaika akaniambia, “Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya harusi ya Mwanakondoo!” Tena akaniambia, “Hayo ni maneno ya kweli ya Mungu.” Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake, nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote tunamshuhudia Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio unaowaangazia manabii.” Kisha, nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi mmoja mweupe, na mpandafarasi wake aliitwa “Mwaminifu” na “Kweli”. Huyo huhukumu na kupigana kwa ajili ya haki. Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani. Alikuwa ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa tu yeye mwenyewe. Alikuwa amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina lake huyo ni “Neno la Mungu”. Majeshi ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na yamevaa mavazi ya kitani, meupe na safi. Upanga mkali hutoka kinywani mwake, na kwa upanga huo atawashinda watu wa mataifa. Yeye ndiye atakayetawala kwa fimbo ya chuma na kuikamua divai katika chombo cha kukamulia zabibu za ghadhabu kuu ya Mungu Mwenye Nguvu. Juu ya vazi lake, na juu ya paja lake, alikuwa ameandikwa jina: “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.” Kisha, nikamwona malaika mmoja amesimama katika jua. Akapaza sauti na kuwaambia ndege wote waliokuwa wanaruka juu angani, “Njoni! Kusanyikeni pamoja kwa karamu kuu ya Mungu. Njoni mkaitafune miili ya wafalme, ya majemadari, ya watu wenye nguvu, ya farasi na wapandafarasi wao; njoni mkaitafune miili ya watu wote: Walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.” Kisha, nikaona yule mnyama pamoja na mfalme wa dunia na askari wao wamekusanyika pamoja kusudi wapigane na yule aliyekuwa ameketi juu ya farasi pamoja na jeshi lake. Lakini huyo mnyama akachukuliwa mateka pamoja na nabii wa uongo aliyekuwa akifanya miujiza mbele yake. (Kwa miujiza hiyo, alikuwa amewapotosha wale waliokuwa na chapa ya huyo mnyama, na ambao walikuwa wameiabudu sanamu yake). Huyo mnyama pamoja na huyo nabii walitupwa wote wawili, wakiwa wazimawazima, ndani ya ziwa linalowaka moto wa madini ya kiberiti. Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule anayepanda farasi. Ndege wote wakajishibisha kwa nyama zao. Kisha, nikamwona malaika mmoja anashuka kutoka mbinguni akiwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akalikamata lile joka — nyoka wa kale, yaani Ibilisi au Shetani — akalifunga kwa muda wa miaka 1,000. Malaika akalitupa kuzimu, akaufunga mlango wa kuingilia huko na kuutia mhuri ili lisiweze tena kuyapotosha mataifa mpaka hapo miaka 1,000 itakapotimia. Lakini baada ya miaka hiyo ni lazima lifunguliwe tena, lakini kwa muda mfupi tu. Kisha nikaona viti vya enzi na watu walioketi juu yake; watu hao walipewa mamlaka ya hukumu. Niliona pia roho za wale waliokuwa wamenyongwa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawa hawakumwabudu yule mnyama na sanamu yake, wala hawakupigwa alama yake juu ya paji za nyuso zao, au juu ya mikono yao. Walipata tena uhai, wakatawala pamoja na Kristo kwa miaka 1,000. (Wale wengine waliokufa hawakupata uhai mpaka miaka 1,000 itimie). Huu ndio ufufuo wa kwanza. Wameneemeka sana, tena heri yao wote wanaoshiriki ufufuo huu wa kwanza. Kifo cha pili hakitakuwa na nguvu juu yao; watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, na watatawala pamoja naye kwa miaka 1,000. Wakati miaka 1,000 itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka gerezani mwake. Basi, atatoka nje, ataanza kuyapotosha mataifa yote yaliyotawanyika kila mahali duniani, yaani Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya pamoja kwa ajili ya vita; nao watakuwa wengi kama mchanga wa pwani. Walipita katika nchi yote, wakaizunguka kambi ya watakatifu na mji wa Mungu aupendao. Lakini moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawaangamiza. Naye Ibilisi aliyekuwa anawapotosha, akatupwa ndani ya ziwa linalowaka madini ya kiberiti, walimo yule mnyama na yule nabii wa uongo, nao watateswa mchana na usiku, milele na milele. Kisha, nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe, na yule aketiye juu yake. Dunia na mbingu vikatoweka mbele ya macho yake, na havikuonekana tena. Kisha nikawaona watu wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa. Halafu kitabu kingine, yaani kitabu cha uhai, kikafunguliwa pia. Wafu wakahukumiwa kadiri ya matendo yao, kama ilivyoandikwa ndani ya vitabu hivyo. Bahari ikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yake; Kifo na Kuzimu vikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yao. Kila mmoja akahukumiwa kufuatana na matendo yake. Kisha Kifo na Kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto. Ziwa hili la moto ndicho kifo cha pili. Mtu yeyote ambaye jina lake halikupatikana limeandikwa katika kitabu cha uhai, alitupwa katika ziwa la moto. Kisha, nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuwako tena. Nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Ulikuwa umetayarishwa vizuri kama bibi arusi aliyepambwa tayari kukutana na mumewe. Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha enzi ikisema, “Tazama! Maskani ya Mungu kati ya watu. Atakaa kati yao, nao watakuwa watu wake, naye atakuwa Mungu wao. Yeye atayafuta machozi yao yote; maana kifo hakitakuwako tena, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!” Kisha yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi akasema, “Tazama, nafanya yote mapya.” Tena akaniambia, “Andika jambo hili, maana maneno haya ni ya kuaminika na ya kweli!” Kisha akaniambia, “Yametimia! Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Aliye na kiu nitampa kinywaji cha bure kutoka katika chemchemi ya maji ya uhai. Mshindi yeyote atapokea hicho, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Lakini watu waoga, wasioamini, wapotovu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, na waongo wote, mahali pao patakuwa ndani ya lile ziwa linalowaka moto na madini ya kiberiti; hicho ndicho kifo cha pili.” Kisha mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba yaliyokuwa yamejaa mabaa saba ya mwisho, akaja na kuniambia, “Njoo! Nami nitakuonesha bibi arusi, mkewe Mwanakondoo!” Basi, Roho akanikumba, naye malaika akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionesha mji mtakatifu, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni, uking'aa kwa utukufu wa Mungu. Mwangaza wake ulikuwa kama wa jiwe la thamani kubwa kama yaspi, angavu kama kioo. Ulikuwa na ukuta mrefu na mkubwa, wenye milango kumi na miwili, na kila mmoja ulilindwa na malaika. Juu ya kila mlango paliandikwa mojawapo ya majina ya makabila kumi na mawili ya Israeli. Kila upande ulikuwa na milango mitatu: Upande wa mashariki milango mitatu, kaskazini milango mitatu, kusini milango mitatu na magharibi milango mitatu. Kuta za mji huo zilikuwa zimejengwa juu ya mawe ya msingi kumi na mawili, na juu ya kila jiwe palikuwa pameandikwa mojawapo ya majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo. Basi, yule malaika aliyekuwa anasema nami alikuwa na kijiti cha dhahabu cha kupimia, kwa ajili ya kuupima huo mji, milango yake na kuta zake. Mji wenyewe ulikuwa wa mraba, upana na urefu wake sawa. Basi, malaika akaupima mji huo kwa kijiti chake: Ulikuwa na urefu, upana na kimo cha kama kilomita 2,400. Kisha akaupima ukuta wake pia; nao ulikuwa mita 60 kwa kipimo cha macho cha kibinadamu ambacho malaika alitumia. Ukuta huo ulikuwa umejengwa kwa mawe mekundu ya thamani, na mji wenyewe ulikuwa umejengwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo. Mawe ya msingi wa ukuta huo yalikuwa yamepambwa kwa kila aina ya mawe ya thamani. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa jiwe la thamani jekundu, la pili johari ya rangi ya samawati, la tatu kalkedoni, la nne zumaridi, la tano sardoniki, la sita akiki, la saba krisolito, la nane zabarajadi, la tisa topazi, la kumi krisopraso, la kumi na moja yasintho, na la kumi na mbili amethisto. Na ile milango kumi na miwili ilikuwa lulu kumi na mbili; kila mlango ulikuwa umetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji ilikuwa imetengenezwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo. Sikuona hekalu katika mji huo, maana Bwana Mungu Mwenye Nguvu na yule Mwanakondoo ndio hekalu lake. Mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, maana utukufu wa Mungu huuangazia, na taa yake ni yule Mwanakondoo. Watu wa mataifa watatembea katika mwanga wake na wafalme wa dunia watauletea utajiri wao. Milango ya mji huo itakuwa wazi mchana wote; maana hakutakuwa na usiku humo. Fahari na utajiri wa watu wa mataifa utaletwa humo ndani. Lakini hakuna chochote kilicho najisi kitakachoingia humo; wala mtu yeyote atendaye mambo ya kuchukiza au ya uongo hataingia humo. Ni wale tu walioandikwa katika kitabu cha uhai cha Mwanakondoo ndio watakaoingia ndani. Kisha malaika akanionesha mto wa maji ya uhai maangavu kama kioo, yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uhai unaozaa matunda mara kumi na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu wa mataifa. Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo. Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na watumishi wake watamwabudu. Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso zao. Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele. Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika wake awaoneshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde. “Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.” Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona, nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionesha mambo hayo, nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu Mungu!” Tena akaniambia, “Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia. Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu.” “Sikiliza!” Asema Yesu, “Naja upesi pamoja na tuzo nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake. Mimi ni Alfa na Omega, wa kwanza na wa mwisho, mwanzo na mwisho.” Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, wapate kuwa na haki ya kula tunda la mti wa uhai, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake. Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji. “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!” Roho na Bibi arusi waseme, “Njoo!” Kila mtu asikiaye hili, na aseme, “Njoo!” Aliye na kiu na aje; anayependa, na achukue maji ya uhai bila malipo. Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang'anya sehemu yake katika ule mti wa uhai, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki. Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: “Kweli naja upesi.” Amina. Njoo Bwana Yesu! Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amina.