Hii ni historia ya ukoo wa Yesu, Masihi. Alitoka katika ukoo wa Daudi, aliyetoka katika ukoo wa Ibrahimu. Ibrahimu alikuwa baba yake Isaka. Isaka alikuwa baba yake Yakobo. Yakobo alikuwa baba wa Yuda na ndugu zake. Yuda alikuwa baba wa Peresi na Zera. (Mama yao alikuwa Tamari.) Peresi alikuwa baba yake Hezroni. Hezroni alikuwa baba yake Ramu. Ramu alikuwa baba yake Aminadabu. Aminadabu alikuwa baba yake Nashoni. Nashoni alikuwa baba yake Salmoni. Salmoni alikuwa baba yake Boazi. (Mama yake Boazi alikuwa Rahabu.) Boazi alikuwa baba yake Obedi. (Mama yake Obedi alikuwa Ruthu.) Obedi alikuwa baba yake Yese. Yese alikuwa baba yake Mfalme Daudi. Daudi alikuwa baba yake Sulemani. (Mama yake Sulemani alikuwa mke wa Uria.) Sulemani alikuwa baba yake Rehoboamu. Rehoboamu alikuwa baba yake Abiya. Abiya alikuwa baba yake Asa. Asa alikuwa baba yake Yehoshafati. Yehoshafati alikuwa baba yake Yoramu. Yoramu alikuwa baba yake Uzia. Uzia alikuwa baba yake Yothamu. Yothamu alikuwa baba yake Ahazi. Ahazi alikuwa baba yake Hezekia. Hezekia alikuwa baba yake Manase. Manase alikuwa baba yake Amoni. Amoni alikuwa baba yake Yosia. Yosia alikuwa baba wa Yekonia na ndugu zake. Walioishi wakati ambao watu walipelekwa utumwani Babeli. Baada ya uhamisho wa Babeli, Yekonia akawa baba yake Shealtieli. Shealtieli alikuwa babu wa Zerubabeli. Zerubabeli alikuwa baba yake Abiudi. Abiudi alikuwa baba yake Eliakimu. Eliakimu alikuwa baba yake Azori. Azori alikuwa baba yake Sadoki. Sadoki alikuwa baba yake Akimu. Akimu alikuwa baba yake Eliudi. Eliudi alikuwa baba yake Eliazari. Eliazari alikuwa baba yake Matani. Matani alikuwa baba yake Yakobo. Yakobo alikuwa baba yake Yusufu, Yusufu alikuwa mume wa Mariamu. Na Mariamu alimzaa Yesu, anayeitwa Masihi. Kulikuwa na vizazi kumi na nne kuanzia kwa Ibrahimu mpaka kwa Daudi. Na kulikuwa na vizazi kumi na nne kuanzia kwa Daudi mpaka wakati wa uhamisho wa Babeli. Na palikuwa na vizazi kumi na nne tangu uhamisho wa Babeli mpaka wakati alipozaliwa Yesu, Masihi. Kuzaliwa kwa Yesu Masihi, kulikuwa hivi: Mariamu mama yake alikuwa amechumbiwa na Yusufu. Kabla hawajaoana, Yusufu aligundua kuwa Mariamu alikuwa mja mzito. (Yeye alipata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.) Kwa kuwa Yusufu alitaka kufanya kile kilichokuwa, alikusudia kumwacha Mariamu kwa siri bila ya kumvunjia heshima. Lakini baada ya Yusufu kuliwazia jambo hili, Malaika wa Bwana alimjia katika ndoto na akamwambia, “Yusufu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Mariamu awe mke wako. Mimba aliyonayo ameipata kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Atamzaa mwana, nawe utamwita Yesu. Utampa jina hilo Yesu kwa sababu yeye atawaokoa watu wake kutoka dhambi zao.” Haya yote yalitokea ili kutimiza maneno ambayo Bwana aliyasema kupitia kwa nabii aliposema: “Sikiliza! Msichana bikira atapata mimba na atazaa mtoto wa kiume. Mtoto huyo ataitwa Emanueli.” (Yaani “Mungu yu pamoja nasi”.) Yusufu alipoamka alifanya kama alivyoelekezwa na Malaika wa Bwana. Alimuoa Mariamu. Lakini hakukutana naye kimwili mpaka Mariamu alipomzaa mwana. Na Yusufu akamwita Yesu. Yesu alizaliwa katika mji wa Bethlehemu ya Uyahudi wakati Herode alipokuwa mfalme. Baada ya Yesu kuzaliwa, baadhi ya wenye hekima kutoka mashariki walikuja Yerusalemu. Walipofika wakawauliza watu, “Yuko wapi mtoto aliyezaliwa ili awe Mfalme wa Wayahudi? Tuliiona nyota ilipochomoza na kutuonesha kuwa amezaliwa. Nasi tumekuja ili tumwabudu.” Mfalme Herode aliposikia haya, yeye pamoja na watu wote wakaao Yerusalemu walikasirika sana. Herode aliitisha mkutano wa wakuu wote wa makuhani wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Akawauliza ni wapi ambapo Masihi angezaliwa. Wakamjibu, “Ni katika mji wa Bethlehemu ya Yuda kama ambavyo nabii aliandika: ‘Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, wewe ni wa muhimu miongoni mwa watawala wa Yuda. Ndiyo, mtawala atakayewaongoza watu wangu Israeli, atatoka kwako.’” Kisha Herode akawaita na kufanya mkutano wa siri na wenye hekima kutoka mashariki. Akaelewa kwa usahihi wakati walipoiona nyota. Kisha akawaruhusu waende Bethlehemu. Akawaambia, “Nendeni mkamtafute mtoto kwa makini na mtakapompata mrudi na kunipa taarifa mahali alipo, ili nami pia niende kumwabudu.” Wenye hekima walipomsikiliza mfalme, waliondoka. Waliiona tena ile nyota waliyoiona hapo mwanzo na wakaifuata. Nyota ile iliwaongoza mpaka mahali alipokuwa mtoto na kusimama juu ya sehemu hiyo. Wenye hekima walipoona kuwa nyota ile imesimama, walifurahi na kushangilia kwa furaha. Wenye hekima hao kisha waliingia katika nyumba alimokuwamo mtoto Yesu pamoja na Mariamu mama yake. Walisujudu na kumwabudu mtoto. Kisha wakafungua masanduku yenye zawadi walizomletea mtoto. Wakampa hazina za dhahabu, uvumba na manemane. Lakini Mungu aliwaonya wenye hekima hao katika ndoto kuwa wasirudi tena kwa Herode. Hivyo kwa kutii walirudi nchini kwao kwa kupitia njia nyingine. Baada ya wenye hekima kuondoka, malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto na kumwambia, “Damka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake ukimbilie Misri kwa sababu Herode amedhamiria kumwua mtoto na sasa atatuma watu kumtafuta. Na mkae Misri mpaka nitakapowaambia mrudi.” Hivyo Yusufu alidamka na kutoka kwenda Misri akiwa na mtoto na mama yake. Nao waliondoka usiku. Yusufu na familia yake walikaa huko Misri mpaka Herode alipofariki. Hili lilitukia ili maneno yaliyosemwa na nabii yatimie: “Nilimwita mwanangu atoke Misri.” Herode alipoona kuwa wenye hekima wamemfanya aonekane mjinga, alikasirika sana. Hivyo akatoa amri ya kuua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili au chini ya miaka hiyo katika mji wa Bethlehemu na vitongoji vyake. Herode alifahamu kutoka kwa wenye hekima kwamba walikuwa wameiona nyota miaka miwili kabla. Hili likatimiza yale yaliyosemwa na Mungu kupitia nabii Yeremia aliposema: “Sauti imesikika Rama, sauti ya kilio na huzuni kuu. Raheli akiwalilia watoto wake, na amekataa kufarijiwa kwa sababu watoto wake hawapo tena.” Wakati Yusufu na familia yake wakiwa Misri, Herode alifariki. Malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto na akamwambia, “Damka! Mchukue mtoto na mama yake urudi Israeli, kwani waliojaribu kumwua mtoto wamekwisha kufa.” Hivyo Yusufu alidamka na kumchukua mtoto Yesu na mama yake na kurudi Israeli. Lakini Yusufu aliposikia kuwa Arkelao alikuwa mfalme wa Yuda baada ya baba yake kufa, aliogopa kwenda huko. Lakini baada ya kuonywa na Mungu katika ndoto, Yusufu aliondoka pamoja na familia yake akaenda sehemu za Galilaya. Alikwenda katika mji wa Nazareti na kukaa huko. Hii ilitokea ili kutimiza maneno yale yaliyosemwa na manabii. Mungu alisema Masihi angeitwa Mnazareti. Baadaye, kabla ya miaka mingi kupita, Yohana Mbatizaji alianza kuwahubiri watu ujumbe uliotoka kwa Mungu. Naye alihubiri kutokea maeneo ya nyikani huko Uyahudi. Yohana alisema, “Tubuni na kuibadili mioyo yenu, kwa sababu ufalme wa Mungu umekaribia.” Nabii Isaya alisema kuhusu habari za Yohana Mbatizaji pale aliposema, “Kuna mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani: ‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana; nyoosheni njia kwa ajili yake.’” Huyo Yohana alivaa mavazi yaliyofumwa kutokana na manyoya ya ngamia. Naye alijifunga mkanda wa ngozi kuzunguka kiuno chake, na alikula nzige na asali mbichi. Watu kutoka Yerusalemu na maeneo yote ya Uyahudi na wale kutoka maeneo yote yaliyo kando ya Mto Yordani walikwenda kwa Yohana Mbatizaji; huko waliungama matendo yao mabaya kwake naye akawabatiza katika Mto Yordani. Mafarisayo na Masadukayo wengi walikwenda kwa Yohana ili wabatizwe. Yohana alipowaona, akasema, “Enyi ninyi nyoka! Ni nani amewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja? Muibadili mioyo yenu! Na muoneshe kwa vitendo kuwa mmebadilika. Ninajua mnachofikiri. Mnataka akasema kuwa, ‘lakini Ibrahimu ni baba yetu!’ Hiyo haijalishi. Ninawaambia Mungu anaweza kumzalia Ibrahimu watoto kutoka katika mawe haya. Shoka limewekwa tayari kukata shina la mti katika mizizi yake. Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa vivyo hivyo na kutupwa motoni. Mimi ninawabatiza kwa maji kuonesha kuwa mmebadilika mioyoni mwenu na pia maishani mwenu. Lakini yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, huyo atafanya mengi zaidi yangu. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Yeye huyo atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Naye atakuja akiwa tayari kwa ajili ya kuisafisha nafaka. Atatenganisha nafaka nzuri kutoka kwenye makapi, na kisha ataiweka nafaka nzuri kwenye ghala yake. Kisha atayachoma makapi kwa moto usiozimika.” Ndipo Yesu alitoka Galilaya na kwenda Mto Yordani. Alikwenda kwa Yohana, akitaka kubatizwa. Lakini Yohana alijaribu kumzuia. Yohana akamwambia Yesu, “Kwa nini unakuja kwangu ili nikubatize? Mimi ndiye ninayepaswa kubatizwa na wewe!” Yesu akajibu, “Acha iwe hivyo kwa sasa. Tunapaswa kuyatimiza mapenzi ya Mungu.” Ndipo Yohana akakubali. Hivyo Yesu akabatizwa. Mara tu aliposimama kutoka ndani ya maji, mbingu zilifunguka na akamwona Roho Mtakatifu akishuka kutoka mbinguni kama hua na kutua juu yake. Sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu, nimpendaye. Ninapendezwa naye.” Kisha Roho Mtakatifu akamwongoza Yesu hadi nyikani ili akajaribiwe na Shetani. Baada ya Yesu kufunga kwa siku arobaini mchana na usiku, akaumwa njaa sana. Mjaribu akamwendea na akasema, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, basi yaamuru mawe haya yawe mikate.” Yesu akajibu, “Maandiko yanasema, ‘Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila Neno linalotoka katika kinywa cha Mungu.’” Kisha Shetani alimwongoza Yesu mpaka mji mtakatifu wa Yerusalemu na akamweka juu ya mnara wa Hekalu. Akamwambia Yesu, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe mpaka chini! Kwani Maandiko yanasema, ‘Mungu atawaamuru malaika zake wakusaidie, na mikono yao itakupokea, ili usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe.’” Yesu akamjibu, “Pia, Maandiko yanasema, ‘usimjaribu Bwana Mungu wako.’” Kisha Shetani akamwongoza Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima ulio mrefu sana na kumwonyesha falme zote za ulimwengu na vitu vya kupendeza vilivyomo ndani. Shetani akamwambia Yesu, “Ukiinama na kuniabudu, nitakupa vitu hivi vyote.” Yesu akamjibu Shetani akamwambia, “Ondoka kwangu Shetani! Kwani Maandiko yanasema, ‘Umwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake!’” Baada ya hayo, Shetani akamwacha. Ndipo malaika wakaja kumhudumia. Yesu aliposikia kuwa Yohana alikuwa amefungwa gerezani, alirudi katika wilaya ya Galilaya. Lakini aliondoka Nazareti. Alikwenda kuishi Kapernaumu, mji ulio kando kando ya Ziwa Galilaya katika eneo la Zabuloni na Naftali. Hili lilitokea ili kutimiza maneno aliyosema nabii Isaya: “Sikilizeni, enyi nchi ya Zabuloni na Naftali, nchi iliyo kando ya barabara iendayo baharini, ng'ambo ya Mto Yordani! Galilaya, wanapokaa Mataifa. Watu wanaoishi katika giza ya kiroho, nao wameiona nuru iliyo kuu. Nuru hiyo imeangaza kwa ajili yao wale wanaoishi katika nchi yenye giza kama kaburi.” Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaambia watu ujumbe wake unaosema, “Mbadili mioyo yenu na maisha yenu pia, kwa sababu Ufalme wa Mungu umewafikia.” Yesu alipokuwa akitembea kando ya Ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni, aitwaye Petro na nduguye aitwaye Andrea. Ndugu hawa walikuwa wavuvi na walikuwa wanavua samaki kwa nyavu zao. Yesu akawaambia, “Njooni, mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa aina nyingine. Nitawafundisha jinsi ya kukusanya watu badala ya samaki.” Mara moja, Simoni na Andrea wakaziacha nyavu zao na kumfuata Yesu papo hapo. Yesu akaendelea kutembea kutoka pale. Akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo. Walikuwa kwenye mashua pamoja na Zebedayo baba yao. Walikuwa wakiandaa nyavu zao za kuvulia samaki. Yesu akawaita wamfuate. Mara moja wakaiacha mashua pamoja na baba yao na wakamfuata Yesu. Yesu alikwenda sehemu zote za Galilaya, akifundisha na akihubiri Habari Njema katika masinagogi kuhusu Ufalme wa Mungu. Aliponya magonjwa yote na madhaifu mengi ya watu. Habari kuhusu Yesu zilienea katika nchi yote ya Shamu, na watu waliwaleta wale wote wenye kuteswa na magonjwa na maumivu mbalimbali. Baadhi yao walikuwa na mashetani, wengine walikuwa na kifafa na wengine walikuwa wamepooza. Yesu akawaponya wote. Makundi makubwa ya watu walimfuata; watu kutoka Galilaya, na jimbo lililoitwa Miji Kumi, Yerusalemu, Yuda na maeneo ng'ambo ya Mto Yordani. Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda kwenye kilima na kukaa chini. Wanafunzi wake walimjia Yesu. Kisha Yesu akaanza kuwafundisha watu kwa akasema: “Heri kwa walio maskini na wenye kujua kwamba wanamhitaji Mungu. Kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wao. Heri kwa wenye huzuni sasa. Kwa kuwa watafarijiwa na Mungu. Heri kwa walio wapole. Kwa kuwa watairithi nchi. Heri kwa wenye kiu na njaa ya kutenda haki. Kwa kuwa Mungu ataikidhi kiu na njaa yao. Heri kwa wanaowahurumia wengine. Kwa kuwa watahurumiwa pia. Heri kwa wenye moyo safi, Kwa kuwa watamwona Mungu. Heri kwa wanaotafuta amani. Kwa kuwa wataitwa watoto wa Mungu. Heri kwa wanaoteswa kwa sababu ya kutenda haki. Kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wao. Heri kwenu ninyi pale watu watakapowatukana na kuwatesa. Watakapodanganya na akasema kila neno baya juu yenu kwa kuwa mnanifuata mimi. Furahini na kushangilia kwa sababu thawabu kuu inawasubiri mbinguni. Furahini kwa kuwa ninyi ni kama manabii walioishi zamani. Watu waliwatendea wao mambo mabaya kama haya pia. Mnahitajika kama chumvi inavyohitajiwa na wale waliopo duniani. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, haiwezi kufanywa chumvi tena. Haina manufaa yo yote isipokuwa hutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru inayong'aa ili ulimwengu uweze kuiona. Ni kama mji uliojengwa juu ya kilima unavyoonekana wazi. Watu hawawashi taa na kuificha kwenye chungu. Bali huiweka kwenye kinara cha taa ili nuru iangaze kwa kila mtu. Kwa namna hiyo hiyo mnapaswa kuwa nuru kwa ajili ya watu wengine. Hivyo ishini katika namna ambayo watakapoyaona matendo yenu mema, watamtukuza Baba yenu wa mbinguni. Msifikiri kwamba nimekuja kuiharibu Sheria ya Musa au mafundisho ya manabii. Sikuja kuyaharibu mafundisho yao bali kuyakamilisha. Ninawahakikishia kuwa hakuna jambo litakaloondolewa katika sheria mpaka mbingu na nchi zitakapopita. Hakuna hata herufi ndogo ama nukta katika Sheria ya Musa itakayotoweka mpaka hapo itakapotimizwa. Kila mtu anapaswa kutii kila amri iliyo katika sheria, hata ile isiyoonekana kuwa ya muhimu. Kila atakayevunja mojawapo ya amri hizi ndogo na kuwafundisha wengine kuzivunja atahesabiwa kuwa ni mdogo sana katika ufalme wa Mungu. Lakini kila anayeitii na kuwafundisha wengine kuitii sheria atakuwa mkuu katika ufalme wa Mungu. Ninawambia, ni lazima muitii sheria ya Mungu kwa kiwango bora kuliko kile cha walimu wa sheria na Mafarisayo. La sivyo, hamtaweza kuingia katika ufalme wa Mungu. Mmesikia kuwa hapo kale baba zetu waliambiwa, ‘Usimwue yeyote. Na yeyote atakayeua atahukumiwa.’ Lakini ninawaambia, msimkasirikie mtu yeyote kwa sababu mkifanya hivyo mtahukumiwa. Na mkimtukana mtu yeyote, vivyo hivyo mtahukumiwa na baraza kuu. Na ukimwita mtu kuwa ni mjinga, utakuwa katika hatari ya kutupwa kwenye moto wa Jehanamu. Unapokwenda kutoa sadaka yako madhabahuni na ukakumbuka kuwa kuna mtu ana jambo dhidi yako. Unapaswa kuiacha sadaka yako kwenye madhabahu na uende kupatana na mtu huyo. Ukiisha patana naye ndipo urudi na kuitoa sadaka hiyo. Akiwepo mtu anayetaka kukushtaki, patana naye haraka. Jitahidi kufanya hivyo kabla ya kufika mahakamani, hata kama bado mpo njiani. Usipofanya hivyo anaweza kukupeleka kwa hakimu. Na hakimu atakupeleka kwa walinzi watakaokufunga gerezani. Ninakuhakikishia kuwa hautatoka huko mpaka umelipa kila kitu unachodaiwa. Mmesikia ilisemwa kuwa, ‘Usizini’. Lakini ninawaambia kuwa mwanaume akimwangalia mwanamke na akamtamani, amekwisha kuzini naye katika akili yake. Jicho la kuume likikufanya utende dhambi, liondoe na ulitupe. Ni bora kupoteza sehemu moja ya mwili wako kuliko mwili wako wote ukatupwa Jehanamu. Na mkono wako wa kuume ukikufanya utende dhambi, uukate na kuutupa. Ni bora kupoteza sehemu moja ya mwili wako kuliko mwili wako wote kutupwa Jehanamu. Ilisemwa pia kuwa, ‘Kila anayemtaliki mkewe ni lazima ampe hati ya talaka.’ Lakini ninawaambia kuwa, kila atakayemtaliki mkewe kutokana na sababu isiyohusiana na uzinzi, anamfanya mke wake kuwa mzinzi. Na kila atakayemwoa mwanamke aliyetalikiwa, atakuwa anazini. Pia, mmesikia hapo kale baba zetu waliambiwa, ‘Unaweka kiapo, usishindwe kutimiza kile ulichoapa kufanya. Timiza kiapo ulichoweka mbele za Bwana.’ Lakini ninawaambia mnapoweka ahadi, msiape kwa jina la mbingu, kwa sababu mbingu ni kiti cha enzi cha Mungu. Na usiape kwa jina la dunia kwa sababu, dunia ni mahali pa kuweka miguu yake. Wala msiape kwa jina la mji wa Yerusalemu, kwa sababu nao ni mali yake Mungu, aliye Mfalme Mkuu. Pia usiape kwa jina la kichwa chako kana kwamba ni uthibitisho kuwa utatimiza kiapo, kwa sababu huwezi kuufanya hata unywele mmoja wa kichwa chako kuwa mweusi au mweupe. Sema ‘ndiyo’ tu kama una maana ya ndiyo na ‘hapana’ tu kama una maana ya hapana. Ukisema zaidi ya hivyo, utakuwa unatoa kwa Yule Mwovu. Mmesikia ilisemwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ Lakini ninawaambia msishindane na yeyote anayetaka kuwadhuru. Mtu akikupiga shavu la kulia mgeuzie na la kushoto pia. Mtu akitaka kukushitaki ili akunyang'anye shati, mpe na koti pia. Askari akikulazimisha kwenda naye maili moja, nenda maili mbili pamoja naye. Mpe kila anayekuomba, usimkatalie anayetaka kuazima kitu kwako. Mmesikia ilisemwa kuwa, ‘Wapende rafiki zako na wachukie adui zako.’ Lakini ninawaambia wapendeni adui zenu na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. Mkifanya hivi mtakuwa watoto halisi walio kama Baba yenu wa mbinguni. Yeye huwaangazia jua watu wote, bila kujali ikiwa ni wema au wabaya. Huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Ikiwa mnawapenda wale wanaowapenda ninyi, kwa nini mpate thawabu toka kwa Mungu? Hata watoza ushuru hufanya hivyo. Na ikiwa mnakuwa wema kwa rafiki zenu tu, ninyi si bora kuliko wengine. Hata watu wasiomjua Mungu ni wakarimu kwa rafiki zao pia. Ninalosema ni kuwa, mkue hata kufikia upendo kamili alionao baba yenu wa Mbinguni kwa watu wote. Mnapofanya jambo jema, kuweni waangalifu msilifanye mbele za watu wengine ili wawaone. Mtakapofanya hivyo hamtapata thawabu kutoka kwa Baba yenu wa mbinguni. Unapowapa maskini na wahitaji, usilipigie mbiu sana jambo hilo. Maana hivyo ndivyo wanavyofanya wanafiki kwenye makusanyiko. Wao hupiga mbiu kabla ya kutoa ili watu wawaone, kwa kuwa hutaka kila mtu awasifu. Ukweli ni kuwa, hiyo ndiyo thawabu yote waliyokwishapata. Hivyo unapowapa maskini, mtu yeyote asijue unachofanya. Kutoa kwako kunapaswa kufanyika sirini kwa kuwa Baba yako huona mambo yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu. Mnapoomba, msiwe kama wanafiki. Wanapenda kusimama kwenye masinagogi na kwenye pembe za mitaa na kuomba kwa kupaza sauti. Wanapenda kuonwa na watu. Ukweli ni kuwa hiyo ndiyo thawabu yote watakayopata. Lakini unapoomba, unapaswa kuingia katika chumba chako cha ndani na ufunge mlango. Kisha mwombe Baba yako aliye mahali pa siri. Yeye anayaona mambo yanayofanyika katika siri na hivyo atakupa thawabu. Na unapoomba usiwe kama watu wasiomjua Mungu. Wao kila wanapoomba wanarudia maneno yale yale, tena na tena, wakidhani kuwa wanapoyarudia maneno hayo mara nyingi watasikiwa na Mungu na kujibiwa maombi yao. Msiwe kama wao. Baba yenu anajua yale mnayohitaji kabla hamjamwomba. Hivyo, hivi ndivyo mnapaswa kuomba: ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako lipewe utukufu. Ufalme wako uje. Mapenzi yako yafanyike hapa dunia, kama yanavyofanyika huko mbinguni. Utupe leo chakula tunachohitaji. Utusamehe dhambi zetu, kama tunavyowasamehe wale wanaotukosea. Usiruhusu tukajaribiwa, lakini utuokoe na Yule Mwovu.’ Mkiwasemehe wengine makosa waliyowatendea, Baba yenu wa mbinguni naye atawasamehe makosa yenu pia. Lakini msipowasamehe wengine, Baba Yenu wa mbinguni hatawasamehe ninyi. Mnapofunga, msijionyeshe kuwa na huzuni kama wanafiki wanavyofanya. Hukunja nyuso zao kwa kuonesha kuwa wana huzuni ili watu wawaone kuwa wamefunga. Ukweli ni kuwa wamekwishapata thawabu yao yote. Hivyo unapofunga, nawa uso wako na ujiweke katika mwonekano mzuri, ili watu wasijue kuwa umefunga, isipokuwa Baba yako, aliye nawe hata sirini. Anaweza kuona yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu. Msijiwekee hazina hapa duniani, mahali nondo na kutu huiharibu. Na wezi wanaweza kuvunja nyumba yako na kuziiba. Badala yake jiwekeeni hazina mbinguni ambako haziwezi kuharibiwa na nondo wala kutu na ambako wezi hawawezi kuvunja na kuziiba. Kwa kuwa roho yako itakuwa mahali ilipo hazina yako. Jinsi unavyowaangalia watu wengine ndivyo inavyoonyesha jinsi wewe mwenyewe ulivyo ndani yako. Ukiwaangalia watu kwa nia njema utajawa na nuru ndani yako. Lakini ukiwaangalia watu kwa nia mbaya, utajawa na giza ndani yako. Na ikiwa yote yanayoonekana ndani yako ni giza peke yake, basi unalo giza baya zaidi! Hamwezi kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Mtamchukia mmoja na kumpenda yule mwingine au mtakuwa waaminifu kwa mmoja na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na pesa. Kwa hiyo ninawaambia, msiyahangaikie mahitaji ya mwili; mtakula nini, mtakunywa nini au mtavaa nini. Uhai ni zaidi ya chakula na mavazi. Waangalieni ndege wa angani. Hawapandi, hawavuni wala kutunza chakula ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, hamjui kuwa ninyi mna thamani zaidi ya ndege? Hamwezi kujiongezea muda wa kuishi kwa kujisumbua. Na kwa nini mna wasiwasi kuhusu mavazi? Yaangalieni maua ya kondeni. Yatazameni namna yanavyomea. Hayafanyi kazi wala kujitengenezea mavazi. Lakini ninawaambia kuwa hata Suleimani, mfalme mkuu na tajiri, hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya maua haya. Ikiwa Mungu anayafanya majani yanayoota mashambani kuwa mazuri mnafikiri atawafanyia ninyi kitu gani? Hayo ni majani tu, siku moja yako hai na siku inayofuata hutupwa katika moto. Lakini Mungu anajali kiasi cha kuyafanya kuwa mazuri ya kupendeza. Muwe na hakika basi atawapa ninyi mavazi mnayohitaji. Imani yenu ni ndogo sana! Msijisumbue na kusema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ Haya ndiyo mambo ambayo watu wasiomjua Mungu huyawazia daima. Msiwe na wasiwasi, kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua kuwa mnayahitaji haya yote. Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na mambo yote ambayo Mungu anahesabu kuwa ni mema na yenye haki. Ndipo Mungu atakapowapa yote mnayohitaji. Msiisumbukie kesho. Kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Kila siku ina mahangaiko yake ya kutosha. Msiwahukumu wengine, ili Mungu asiwahukumu ninyi pia. Mtahukumiwa jinsi ile ile mnavyowahukumu wengine. Mungu atawatendea kama mnavyowatendea wengine. Kwa nini unaona vumbi iliyo katika jicho la rafiki yako, na hujali kipande cha mti kilicho katika jicho lako? Kwa nini unamwambia rafiki yako, ‘Ngoja nitoe vumbi lililo katika jicho lako wakati wewe mwenyewe bado una kipande cha mti katika jicho lako?’ Ewe mnafiki! Ondoa kwanza kipande cha mti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utaweza kuona vizuri na kutoa vumbi katika jicho la rafiki yako. Msiwape mbwa kitu kitakatifu, watawageuka na kuwadhuru. Na msiwatupie nguruwe lulu zenu kwa kuwa watazikanyaga tu. Endeleeni kumwomba Mungu, naye atawapa, endeleeni kutafuta nanyi mtapata, endeleeni kubisha nanyi mtafunguliwa mlango. Ndiyo, yeyote anayeendelea kuomba atapokea. Yeyote anayeendelea kutafuta atapata. Na yeyote anayeendelea kubisha atafunguliwa mlango. Ni nani kati yenu aliye na mwana ambaye akimwomba mkate atampa jiwe? Au akimwomba samaki, atampa nyoka? Bila shaka hakuna! Ijapokuwa ninyi watu ni waovu, lakini bado mnajua kuwapa vitu vyema watoto wenu. Hakika Baba yenu wa mbinguni atawapa vitu vyema wale wamwombao. Watendee wengine kama ambavyo wewe ungetaka wao wakutendee. Hii ndiyo tafsiri ya torati na mafundisho ya manabii. Unapaswa kuingia katika uzima wa kweli kupitia lango lililo jembamba. Kwa kuwa lango ni pana na njia inayoelekea katika uharibifu nayo ni pana na watu wengi wanaifuata njia hiyo. Lakini lango la kuelekea katika uzima wa kweli ni jembamba. Na njia iendayo huko ni ngumu kuifuata. Na ni watu wachache wanaoiona. Mjihadhari na manabii wa uongo wanaokuja kwenu wakijifanya kondoo wasio na madhara ingawa ni watu hatari kama mbwa mwitu. Mtawatambua watu hawa kwa matendo yao. Mambo mazuri hayatoki kwa watu wabaya, kama ambavyo zabibu haitokani na miiba, na tini hazitokani na mbigiri. Vile vile, kila mti mzuri huzaa matunda mazuri na mti mbaya huzaa matunda mabaya. Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, na wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa kwenye moto. Mtawatambua manabii hawa wa uongo kwa matendo yao. Si kila aniitaye Bwana ataingia katika ufalme wa Mungu. Watakaoingia ni wale tu wafanyao yale ambayo Baba yangu wa mbinguni anataka. Siku ya mwisho wengi wataniiita Bwana. Watasema, ‘Bwana, kwa nguvu za jina lako tulihubiri. Na kwa nguvu za jina lako tulitoa mashetani na kufanya miujiza mingi.’ Ndipo nitawaambia waziwazi, ‘Ondokeni kwangu, ninyi waovu. Sikuwahi kuwajua.’ Kila anayeyasikia mafundisho yangu na kuyatii ni kama mwenye hekima aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. Mvua kubwa iliponyesha na mafuriko yakaja, na upepo ukavuma sana, na kuipiga sana nyumba yake. Lakini, nyumba yake haikuanguka kwa sababu ilijengwa kwenye mwamba. Lakini kila anayeyasikia mafundisho yangu na asiyatii ni kama mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. Mvua kubwa iliponyesha na mafuriko kuja, na upepo ukavuma sana, nyumba yake ilianguka kwa kishindo kikuu.” Yesu alipomaliza kufundisha, watu walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka. Yesu alipotelemka kutoka kwenye kilima, umati mkubwa wa watu ulimfuata. Mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea, akainama mbele yake mpaka chini na akasema, “Bwana ukitaka una uwezo wa kuniponya.” Yesu aliunyoosha mkono wake akamshika mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Akasema, “Hakika, ninataka kukuponya. Upone!” Mtu huyo akapona ugonjwa mbaya sana wa ngozi saa hiyo hiyo. Kisha Yesu akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea, lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze. Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona.” Yesu alikwenda Kapernaumu. Alipoingia mjini, afisa wa jeshi alimjia na kumwomba msaada. Akasema, “Bwana, mtumishi wangu ni mgonjwa sana nyumbani na amelala kitandani. Hawezi hata kutingishika na ana maumivu makali sana.” Yesu akamwambia yule afisa, “Nitakwenda nimponye.” Yule afisa akajibu, “Bwana, mimi si mwema kiasi cha wewe kuingia katika nyumba yangu. Toa amri tu, na mtumishi wangu atapona. Ninajua hii, kwa kuwa ninaelewa mamlaka. Kuna watu wenye mamlaka juu yangu, na nina askari walio chini ya mamlaka yangu. Nikimwambia askari mmoja ‘nenda’, huenda. Na nikimwambia mwingine ‘njoo’, huja. Pia nikimwambia mtumwa wangu ‘fanya hiki’, hunitii.” Yesu aliposikia maneno hayo alishangaa. Akawaambia wale waliokuwa wakifuatana naye, “Ukweli ni kuwa, mtu huyu ana imani kuliko mtu yeyote niliyewahi kumwona katika Israeli. Watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi na kula pamoja na Ibrahimu, Isaka, na Yakobo katika ufalme wa Mungu. Na wale wanaopaswa kuwa katika ufalme watatupwa nje gizani. Na huko watalia na kusaga meno yao kwa sababu ya maumivu.” Kisha Yesu akamwambia yule afisa, “Rudi nyumbani kwako. Mtumishi wako atapona kama unavyoamini.” Mtumishi wa afisa huyo akapona wakati ule ule. Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wake Petro amelala kitandani akiwa na homa. Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, kisha akasimama na kuanza kumhudumia. Ilipofika jioni, watu wengi waliokaliwa na mashetani waliletwa kwa Yesu. Naye aliyaamuru mashetani hayo kuwaacha watu. Na aliowaponya wagonjwa wote. Hii ilitokea ili kutimiza maneno yaliyosemwa na nabii Isaya aliposema: “Aliyaondoa magonjwa yetu na kuyabeba madhaifu yetu.” Yesu alipoona kundi la watu waliomzunguka, aliawaambia wafuasi waende upande mwingine wa ziwa. Kisha, mwalimu wa sheria ya Musa akamwendea na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata kila mahali utakapokwenda.” Yesu akamwambia, “Mbweha wana mashimo wanamoishi, ndege wana viota. Lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kupumzika.” Mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana mimi pia nitakufuata, lakini niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.” Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate mimi, na uwaache wale waliokufa wawazike wafu wao.” Yesu alipanda mashua pamoja na wanafunzi wake. Baada ya mashua kutoka pwani, upepo wenye nguvu sana ukaanza kuvuma ziwani. Mawimbi yakaifunika mashua. Lakini Yesu alikuwa amelala. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha. Wakamwambia, “Bwana tuokoe! Tutazama majini!” Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Hamna imani ya kutosha.” Yesu akasimama akaukemea upepo na mawimbi, na ziwa likatulia. Wanafunzi wake wakashangaa sana, wakasema, “Huyu ni mtu wa namna gani? Hata upepo na maji vinamtii!” Yesu alifika ng'ambo ya ziwa katika nchi walimoishi Wagadarini. Hapo wanaume wawili waliokuwa na mashetani ndani yao na kuishi makaburini walimwijia Yesu. Watu hao walikuwa hatari sana na watu hawakuitumia njia iliyopita karibu na makaburi yale. Wakapaza sauti na akasema, “Unataka nini kwetu, Mwana wa Mungu? Umekuja kutuadhibu kabla ya wakati uliopangwa?” Mbali kidogo na mahali hapo lilikuwepo kundi la nguruwe waliokuwa wanapata malisho yao. Mashetani yakamsihi Yesu yakasema, “Ikiwa utatufukuza kutoka ndani ya watu hawa, tafadhali tuache tuwaingie wale nguruwe.” Ndipo akawaamuru na akasema, “Nendeni!” Wale mashetani wakatoka ndani ya wale watu na kuwaingia nguruwe. Kisha kundi lote la nguruwe likaporomoka ziwani na nguruwe wote wakazama na kufa. Wachungaji waliokuwa wakiwachunga wale nguruwe wakakimbia. Wakaenda mjini na kuwaambia watu kila kitu kilichotukia, hasa juu ya wanaume wale wawili waliokuwa na mashetani. Kisha watu wote mjini walikwenda kumwona Yesu. Walipomwona, walimsihi aondoke katika eneo lao. Yesu akapanda katika mashua na akasafiri kwa kukatisha ziwa kurudi kwenye mji wake. Baadhi ya watu wakamletea mtu aliyepooza akiwa amelala kwenye machela. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Changamka mtoto wangu! Dhambi zako zimesamehewa.” Baadhi ya walimu wa sheria walisikia alichosema Yesu. Wakaambizana wao kwa wao, “Si anamtukana Mungu mtu huyu akasema hivyo!” Yesu alipotambua walichokuwa wanafikiri, akasema, “Kwa nini mna mawazo maovu kama hayo mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa.’ Kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kitanda chako na utembee’? Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina.” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kitanda chako uende nyumbani!’” Mtu yule akasimama na kwenda nyumbani. Watu walipoliona tukio hili wakashangaa. Wakamsifu Mungu kwa kuwapa watu mamlaka hii. Yesu alipokuwa anaondoka, alimwona mtu aliyeitwa Mathayo amekaa mahali pa kukusanyia ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Hivyo Mathayo akasimama na kumfuata Yesu. Baadaye Yesu alikula chakula nyumbani kwa Mathayo. Watoza ushuru wengi na watu wenye sifa mbaya walikuja na kula chakula pamoja na Yesu pamoja na wafuasi wake. Mafarisayo walipoona kuwa Yesu anakula pamoja na watu hao, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?” Yesu alipowasikia wakisema hili, akawaambia, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari si wenye afya. Nendeni mkajifunze andiko hili linamaanisha nini: ‘Sihitaji dhabihu ya mnyama; Ninataka ninyi mwoneshe wema kwa watu.’ Sikuja kuwaalika wema kujiunga nami, bali wenye dhambi.” Kisha wafuasi wa Yohana wakamjia Yesu na kusema, “Sisi na Mafarisayo tunafunga mara kwa mara, lakini wafuasi wako hawafungi. Kwa nini?” Yesu akajibu, “Kwenye harusi marafiki wa bwana harusi hawana huzuni anapokuwa pamoja nao, hivyo hawawezi kufunga. Lakini wakati unakuja ambao bwana harusi ataondolewa kwao. Ndipo watakuwa na huzuni kisha watafunga. Mtu anaposhona kiraka kwenye vazi la zamani, atatumia kiraka chakavu. Akitumia kiraka kipya vazi lake litachanika kwa sababu ya kusinyaa kwa kiraka hicho kipya. Kisha tundu litakuwa baya zaidi. Pia, watu hawawaweki divai mpya kwenye viriba vya zamani. Wakifanya hivyo viriba vitapasuka, na divai itamwagika na viriba vitaharibika. Daima watu huweka divai mpya katika viriba vipya, ambavyo haviwezi kupasuka, na divai huwa salama.” Yesu alipokuwa bado anaongea, kiongozi wa sinagogi akamwendea. Kiongozi akainama chini mbele yake na akasema, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini ikiwa utakuja na kumgusa kwa mkono wako, atafufuka.” Hivyo Yesu na wafuasi wake wakaenda na mtu huyo. Wakiwa njiani, alikuwepo mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili. Alimwendea Yesu kwa nyuma na akagusa sehemu ya chini ya vazi lake. Aliwaza, “Ikiwa nitagusa tu joho lake, nitapona.” Yesu aligeuka na kumwona mwanamke. Akasema, “Uwe na furaha, mwanamke. Imani yako imekuponya.” Kisha yule mwanamke akapona saa ile ile. Yesu aliendelea kwenda na kiongozi wa Kiyahudi na kuingia nyumbani kwake. Aliwaona watu wapigao muziki kwa ajili ya mazishi pale. Na aliliona kundi la watu waliohuzunika sana. Yesu akasema, “Ondokeni. Msichana hajafa. Amelala tu.” Lakini watu wakamcheka. Baada ya watu kutolewa nje ya nyumba, Yesu aliingia kwenye chumba cha msichana. Aliushika mkono wa msichana na msichana akasimama. Habari kuhusu jambo hili ilienea kila mahali katika eneo lile. Yesu alipokuwa anaondoka kutoka pale, wasiyeona wawili walimfuata. Walisema kwa sauti, “Mwana wa Daudi, uwe mwema kwetu.” Baada ya Yesu kuingia ndani, wasiyeona wakamwendea. Akawauliza, “Mnaamini kuwa ninaweza kuwafanya muone?” Wakajibu, “Ndiyo, Bwana, tunaamini.” Kisha Yesu akayagusa macho yao na akasema, “Kwa kuwa mnaamini kuwa ninaweza kuwafanya muone, hivyo itatokea.” Ndipo wakaweza kuona. Yesu akawaonya kwa nguvu. Akasema, “Msimwambie yeyote kuhusu hili.” Lakini waliondoka na kutawanya habari kuhusu Yesu kila mahali katika eneo lile. Watu hawa wawili walipokuwa wanaondoka, baadhi ya watu walimleta mtu mwingine kwa Yesu. Mtu huyu alikuwa haongei kwa sababu alikuwa na pepo ndani yake. Yesu akamtoa nje pepo na mtu yule aliweza kuongea. Watu walishangaa na akasema, “Hakuna mtu yeyote aliyewahi kuona kitu kama hiki katika Israeli.” Lakini Mafarisayo walisema, “Mtawala wa mashetani ndiye anayempa nguvu ya kuyatoa mashetani.” Yesu alisafiri akipita katika miji yote na vijiji. Alifundisha katika masinagogi yao na kuwaeleza watu Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Aliponya kila aina ya magonjwa na udhaifu. Yesu aliona watu wengi na kuwahurumia kwa sababu walikuwa wanakandamizwa na hawakuwa na tumaini; kama kondoo bila mchungaji wa kuwaongoza. Yesu akawaambia wafuasi wake, “Kuna mavuno mengi ya watu ya kuleta. Lakini kuna wafanyakazi wachache wa kusaidia kuwavuna. Mungu anamiliki mavuno. Mwombeni atume wafanyakazi wengi zaidi wa kusaidia kukusanya mavuno yake.” Yesu aliwaita pamoja wafuasi wake kumi na mbili. Akawapa uwezo juu ya pepo wabaya ili waweze kuwafukuza na pia kuponya kila aina ya magonjwa na maradhi. Haya ni majina ya mitume kumi na wawili: Simoni (ambaye pia aliitwa Petro), Andrea, kaka yake Petro, Yakobo, mwana wa Zebedayo, Yohana, kaka yake Yakobo, Filipo, Bartholomayo, Thomaso, Mathayo, mtoza ushuru, Yakobo, mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mzelote, Yuda Iskariote (yule ambaye baadaye alimsaliti Yesu). Yesu aliwatuma mitume hawa kumi na wawili pamoja na maelekezo haya: “Msiende kwa watu wasio Wayahudi. Na msiingie katika miji ambako Wasamaria wanaishi. Lakini nendeni kwa watu wa Israeli. Wako kama kondoo waliopotea. Mtakapokwenda, waambieni hivi: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’ Waponyeni wagonjwa. Fufueni waliokufa. Waponyeni watu wenye magonjwa mabaya sana ya ngozi. Na toeni mashetani kwa watu. Ninawapa nguvu hii bure, hivyo wasaidieni wengine bure. Msibebe pesa pamoja nanyi; dhahabu au fedha au shaba nyekundu. Msibebe mikoba. Chukueni nguo na viatu mlivyovaa tu. Na msichukue fimbo ya kutembelea. Mfanyakazi anastahili kupewa anachohitaji. Mnapoingia katika mji, tafuteni kwa makini hadi mumpate mtu anayefaa na mkae katika nyumba yake mpaka mtakapoondoka mjini. Mtakapoingia katika nyumba hiyo, semeni, ‘Amani iwe kwenu.’ Ikiwa watu katika nyumba hiyo watawakaribisha, wanastahili amani yenu. Wapate amani mliyowatakia. Lakini ikiwa hawatawakaribisha, hawastahili amani yenu. Ichukueni amani mliyowatakia. Na ikiwa watu katika nyumba au mji watakataa kuwapokea au kuwasikiliza, basi ondokeni mahali hapo na mkung'ute mavumbi kutoka katika miguu yenu. Ninaweza kuwathibitishia kuwa siku ya hukumu itakuwa vibaya sana kwa mji huo kuliko watu wa Sodoma na Gomora. Sikilizeni! Ninawatuma, nanyi mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Hivyo muwe na akili kama nyoka. Lakini pia muwe kama njiwa na msimdhuru yeyote. Muwe waangalifu! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka ili kuwashitaki mbele ya mabaraza ya mijini. Watawachapa ndani ya masinagogi yao. Mtasimamishwa mbele ya magavana na wafalme. Watu watawafanyia ninyi hivi kwa sababu mnanifuata. Mtakuwa mashahidi wangu mbele za wafalme na magavana hao na kwa watu wa mataifa mengine. Mtakapokamatwa, msisumbuke kuhusu nini mtakachosema au namna gani mtakavyosema. Katika wakati huo mtapewa maneno ya kusema. Si ninyi mtakaoongea; Roho wa Baba Mungu wenu atakuwa anaongea kupitia ninyi. Ndugu watakuwa kinyume cha ndugu zao wenyewe na kuwapeleka kwenda kuuawa. Baba watawapeleka watoto wao wenyewe kuuawa. Watoto watapigana kinyume na wazazi wao na watawapeleka kuuawa. Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. Lakini atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. Mnapotendewa vibaya katika mji mmoja, nendeni katika mji mwingine. Ninawaahidi kuwa hamtamaliza kwenda katika miji ya Israeli kabla Mwana wa Adamu hajarudi. Wanafunzi si wazuri kuliko mwalimu wao. Watumwa si wazuri kuliko bwana wao. Inatosha kwa wanafunzi kuwa kama walimu wao na watumwa kuwa kama bwana wao. Iwapo watu hao wananiita ‘mtawala wa pepo’, na mimi ni kiongozi wa familia, basi ni dhahiri kwa kiasi gani watawatukana ninyi, mlio familia yangu! Hivyo msiwagope watu hao. Kila kitu kilichofichwa kitaoneshwa. Kila kilicho siri kitajulikana. Ninayowaambia ninyi faraghani myaseme hadharani. Kila ninachowanong'oneza nawataka mkiseme kwa sauti kila mtu asikie. Msiwaogope watu. Wanaweza kuua mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Mnapaswa kumwogopa Mungu, anayeweza kuuharibu mwili na roho jehanamu. Ndege wanapouzwa, ndege wawili wadogo hugharimu senti moja tu. Lakini hakuna hata mmoja wa ndege hao wadogo anaweza kufa bila Baba yenu kufahamu. Mungu anafahamu idadi ya nywele katika vichwa vyenu. Hivyo msiogope. Mna thamani kuliko kundi kubwa la ndege. Iwapo mtawaambia watu wengine kuwa mnaniamini, nitamwambia Baba yangu aliye mbinguni kuwa ninyi ni wangu. Lakini ikiwa mtasimama mbele ya wengine na kusema kuwa hamniamini, nitamwambia Baba yangu aliye mbinguni kuwa ninyi si wangu. Msidhani kuwa nilikuja duniani kuleta amani. Sikuja kuleta amani. Nilikuja kuleta vita. Nimekuja ili hili litokee: ‘Mwana atamgeuka baba yake. Binti atamgeuka mama yake. Binti mkwe atamgeuka mama mkwe wake. Hata watu wa familia zenu watakuwa adui zenu.’ Wale wanaowapenda baba zao au mama zao kuliko wanavyonipenda mimi hawana thamani kwangu. Na wale wanaowapenda wana wao au binti zao kuliko wanavyonipenda mimi hawastahili kuwa wafuasi wangu. Wale ambao hawataupokea msalaba waliopewa wanaponifuata hawastahili kuwa wanafunzi wangu na kunifuata. Wale wanaojaribu kuyatunza maisha waliyonayo, watayapoteza. Lakini wale wanaoyaacha maisha yao kwa ajili yangu watapata uzima halisi. Yeyote anayewakubali ninyi ananikubali mimi. Na yeyote anayenikubali anamkubali yule aliyenituma. Yeyote anayemkubali nabii kwa sababu ni nabii atapata ujira wa nabii. Na yeyote anayemkubali mwenye haki kwa sababu ni mwenye haki atapata ujira anaoupata mwenye haki. Yeyote anayemsaidia mmoja wa wafuasi wangu hawa wanyenyekevu kwa sababu ni wafuasi wangu hakika atapata ujira, hata ikiwa wanawapa tu kikombe cha maji baridi.” Yesu alipomaliza maelekezo haya kwa wafuasi wake kumi na wawili wa karibu, aliondoka mahali pale. Akaenda katika miji ya Galilaya kuwafundisha watu na kuwaeleza ujumbe wa Mungu. Yohana alipokuwa gerezani, alisikia kuhusu mambo yaliyokuwa yanatokea; mambo ambayo Masihi angefanya. Hivyo akawatuma baadhi ya wafuasi wake kwa Yesu. Wakamuuliza, “Wewe ni yule tuliyekuwa tunamngojea, au tumsubiri mwingine?” Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mliyosikia na kuona: Vipofu wanaona. Viwete wanatembea. Watu wenye magonjwa ya ngozi wanaponywa. Wasiyesikia wanasikia. Wafu wanafufuliwa. Na habari njema inahubiriwa kwa maskini. Heri ni kwa wale wasio na shida kunikubali.” Wafuasi wa Yohana walipoondoka, Yesu alianza kuongea na watu kuhusu Yohana. Alisema, “Ninyi watu mlikwenda jangwani kuona nini? Mtu aliye dhaifu, kama unyasi unaoyumbishwa na upepo? Hakika, ni nini mlichotarajia kuona? Aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hivyo. Watu wote wanaovaa mavazi mazuri wanapatikana katika ikulu za wafalme. Hivyo mlitoka kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yeye ni zaidi ya hilo. Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana: ‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako. Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’ Ukweli ni kuwa Yohana Mbatizaji ni mkuu kuliko yeyote aliyewahi kuja katika ulimwengu huu. Lakini hata mtu asiye wa muhimu katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana. Tangu wakati wa Yohana Mbatizaji ulipokuja mpaka sasa, Ufalme wa Mungu umekabiliwa na mashambulizi. Watu wenye nguvu wamejaribu kuudhibiti ufalme huu. Kabla ya Yohana kuja, Sheria ya Musa na manabii wote wamesema kuhusu mambo ambayo yangetokea. Na ikiwa mnaamini waliyosema, basi Yohana ni Eliya. Ndiye waliyesema angekuja. Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni! Ninaweza kusema nini kuhusu watu wanaoishi leo? Watu siku ya leo ni kama watoto wanaokaa katika masoko. Kundi moja la watoto linaliambia kundi lingine, ‘Tuliwapigia filimbi, lakini hamkucheza; tuliimba wimbo wa maziko, lakini hamkuhuzunika.’ Kwa nini ninasema watu wako hivyo? Kwa sababu Yohana alikuja na hakula vyakula vya kawaida na kunywa divai, na watu walisema, ‘Ana pepo ndani yake.’ Mwana wa Adamu amekuja akila na kunywa, na watu husema, ‘Mwangalie! Hula sana na kunywa divai nyingi. Ni rafiki wa wakusanya kodi na wenye dhambi wengine.’ Lakini hekima inaonesha kuwa sahihi kutokana na yale inayotenda.” Kisha Yesu akaanza kuikosoa miji ambako alifanya miujiza yake mingi. Aliikosoa miji hii kwa sababu watu katika miji hii hawakubadili maisha yao na kuacha kutenda dhambi. Yesu alisema, “Itakuwa vibaya kwako Korazini! Itakuwa vibaya kwako Bethsaida! Ikiwa miujiza hii hii ingetokea Tiro na Sidoni, watu huko wangeshabadili maisha yao kitambo. Wangekwishavaa magunia na kujimwagia majivu kuonesha kuwa wanasikitikia dhambi zao. Lakini ninawaambia, siku ya hukumu itakuwa vibaya zaidi kwako kuliko Tiro na Sidoni. Nawe Kapernaumu, utakwezwa mpaka mbinguni? Hapana! Utatupwa chini mpaka Kuzimu. Nimetenda miujiza mingi ndani yako. Iwapo miujiza hii ingetokea Sodoma, watu huko wangeacha kutenda dhambi na ungekuwa bado ni mji hata leo. Lakini ninakuambia, itakuwa vibaya kwako siku ya hukumu kuliko Sodoma.” Kisha Yesu akasema, “Ninakusifu wewe, Baba, Bwana wa mbinguni na duniani. Ninashukuru kwa sababu umeyaficha mambo haya kwa wale wanaofikiri kuwa ni wenye hekima na werevu sana. Lakini umeyaonesha haya kwa watu walio kama watoto wadogo. Ndiyo, Baba, ulifanya hivi kwa sababu hakika ndivyo ulivyotaka kufanya. Baba yangu amenipa kila kitu. Hakuna amjuaye Mwana isipokuwa Baba peke yake. Na hakuna amjuaye Baba isipokuwa Mwana ndiye anayemjua Baba. Na watu pekee watakaomjua Baba ni wale ambao Mwana atachagua kuwaonesha. Njooni kwangu ninyi nyote mliochoka kutokana na mizigo mizito mnayolazimishwa kubeba. Nitawapa pumziko. Chukueni nira yangu, jifunzeni kutoka kwangu. Mimi ni mwema na mnyenyekevu katika roho. Nanyi mtaweza kupumzika. Ndiyo, nira yangu ni rahisi. Mzigo ninaowapa muubebe ni mwepesi.” Katika wakati huo huo, Yesu alikuwa anasafiri akipita katika mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wafuasi wake walikuwa pamoja naye, na walikuwa na njaa. Hivyo walianza kuchuma nafaka na kula. Mafarisayo walioliona hili, wakamwambia Yesu, “Tazama! Wafuasi wako wanafanya kitu ambacho ni kinyume na sheria yetu kufanya katika siku ya Sabato.” Yesu akawaambia, “Mmekwisha soma alichofanya Daudi wakati yeye na wale waliokuwa pamoja naye walipokuwa na njaa. Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu. Yeye na wale waliokuwa pamoja naye walikula mkate uliotolewa kwa Mungu. Ilikuwa kinyume cha sheria kwa Daudi au wale waliokuwa pamoja naye kula mkate huo. Makuhani pekee ndio walioruhusiwa kuula. Na mmekwisha soma katika Sheria ya Musa kuwa katika kila Sabato makuhani kwenye Hekalu wanavunja Sheria kwa kufanya kazi Siku ya Sabato. Lakini hawakosei kwa kufanya hivyo. Ninawaambia kuwa kuna kitu hapa ambacho ni kikuu kuliko Hekalu. Maandiko yanasema, ‘Sihitaji dhabihu ya wanyama; Ninataka ninyi muoneshe wema kwa watu.’ Hakika hamjui hilo linamaanisha nini. Iwapo mngelielewa, msingewahukumu wale ambao hawajafanya chochote kibaya. Mwana wa Adamu ni Bwana juu ya siku ya Sabato.” Kutoka hapo Yesu alikwenda katika sinagogi lao. Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepooza mkono. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pale walikuwa wanatafuta sababu ya kumshitaki Yesu kwa kutenda kitu kibaya, hivyo walimuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?” Yesu akajibu, “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo na akatumbukia shimoni siku ya Sabato, utamsaidia kumtoa yule kondoo katika shimo. Hakika mtu ni bora kuliko kondoo. Hivyo ni sawa kutenda wema siku ya Sabato.” Kisha Yesu akamwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “Unyooshe mkono wako.” Mtu yule akaunyoosha mkono wake, na ukawa mzima tena, kama mkono mwingine. Lakini Mafarisayo waliondoka na wakaweka mipango ya kumuua Yesu. Yesu alitambua kuwa Mafarisayo walikuwa wanapanga kumuua. Hivyo aliondoka mahali pale na watu wengi walimfuata. Akawaponya wote waliokuwa wagonjwa, lakini aliwaonya wasiwaambie wengine yeye alikuwa nani. Hii ilikuwa ni kuthibitisha kile ambacho nabii Isaya alisema alipozungumza kwa niaba ya Mungu: “Hapa ni mtumishi wangu, niliyemchagua. Ndiye ninayempenda, na ninapendezwa naye. Nitamjaza Roho yangu, naye ataleta haki kwa mataifa. Hatabishana au kupiga kelele; hakuna atakayesikia sauti yake mitaani. Hatavunja wala kupindisha unyasi. Hatazimisha hata mwanga hafifu. Hatashindwa mpaka ameifanya haki kuwa mshindi. Watu wote watatumaini katika yeye.” Kisha baadhi ya watu wakamleta mtu kwa Yesu. Mtu huyu alikuwa asiyeona na hakuweza kuzungumza, kwa sababu alikuwa na pepo ndani yake. Yesu akamponya na akaweza kuzungumza na kuona. Watu wote walikishangaa kile Yesu alichotenda. Walisema, “Pengine ni Mwana wa ahadi wa Daudi!” Mafarisayo waliposikia hili, walisema, “Mtu huyu anatumia nguvu za Shetani kufukuza mashetani kutoka kwa watu. Beelzebuli ni mtawala wa mashetani.” Yesu alijua kile Mafarisayo walikuwa wanafikiri. Hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe utateketezwa. Na kila mji au familia iliyogawanyika haiwezi kuishi. Hivyo ikiwa Shetani anayafukuza mashetani yake mwenyewe, anapigana kinyume chake yeye mwenyewe, na ufalme wake hautaishi. Mnasema kuwa ninatumia nguvu za Shetani kuyatoa mashetani. Ikiwa hiyo ni kweli, sasa ni nguvu gani watu wenu hutumia wanapoyafukuza mashetani? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa mmekosea. Lakini ninatumia nguvu ya Roho wa Mungu kuyafukuza mashetani, na hili linaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu. Watu wowote wanaotaka kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuiba vitu vyake lazima wamfunge kwanza. Kisha wanaweza kuiba vitu kutoka katika nyumba yake. Yeyote ambaye hayuko pamoja nami yu kinyume nami. Na yeyote ambaye hakusanyi pamoja nami hutawanya. Hivyo ninawaambia, Mungu atawasamehe watu kila dhambi wanayotenda au kila jambo baya wanalosema kinyume naye. Lakini yeyote anayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa. Unaweza kusema kinyume na Mwana wa Adamu na ukasamehewa. Lakini yeyote anayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa; si sasa au baadaye. Ikiwa unataka matunda mazuri, ni lazima uutunze mti vizuri. Ikiwa mti wako siyo mzuri, utakuwa na matunda mabaya. Mti unajulikana kutokana na aina ya matunda inaozalisha. Ninyi nyoka! Ni waovu sana. Mnawezaje mkasema chochote kilicho chema? Kile ambacho watu husema kwa midomo yao kinatoka katika yale yaliyojaa katika mioyo yao. Walio wema wana vitu vizuri vilivyotunzwa katika mioyo yao. Ndiyo maana husema mambo mazuri. Lakini wale walio waovu wana mioyo iliyojaa uovu, na ndiyo sababu husema mambo maovu. Ninawaambia kuwa kila mmoja atajibu kwa ajili ya mambo yasiyo ya maana waliyosema. Hili litatokea siku ya hukumu. Maneno yenu yatatumika kuwahukumu ninyi. Uliyosema yataamua ikiwa una haki mbele za Mungu au unahukumiwa na Mungu.” Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamjibu Yesu. Wakasema, “Mwalimu, tunataka kukuona ukifanya miujiza kama ishara kuwa unatoka kwa Mungu.” Yesu akajibu, “Watu wenye dhambi na wasio na imani hutafuta kuona muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika kudhibitisha chochote kwao. Yona ni ishara pekee itakayotolewa kwenu ninyi mlio wa kizazi kiovu cha leo. Yona alikuwa ndani ya tumbo la samaki mkubwa kwa siku tatu, mchana na usiku. Vivyo hivyo, Mwana wa Adamu atakuwa kaburini kwa siku tatu, mchana na usiku. Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi leo mtalinganishwa na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha namna mlivyokosea. Kwa nini ninasema hivi? Kwa sababu Yona alipowahubiri watu hao, walibadili maisha yao. Na aliye mkuu kuliko Yona, yupo hapa lakini mnakataa kubadilika! Pia, siku ya hukumu, Malkia wa Kusini atasimama pamoja na wale wanaoishi sasa, atasababisha mhukumiwe kuwa na makosa. Ninasema hivi kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana kuja kusikiliza mafundisho yenye hekima ya Sulemani. Nami Ninawaambia aliye mkuu zaidi ya Sulemani yuko hapa, lakini hamnisikii! Roho chafu inapotoka kwa mtu, husafiri katika sehemu kavu ikitafuta mahali pa kupumzika, lakini haipati mahali pa kupumzika. Inapokosa mahali pa kupumzika, husema, ‘Nitarudi katika nyumba niliyotoka.’ Inaporudi, ikakuta nyumba hiyo bado ni tupu, ikiwa safi na nadhifu, hutoka nje na kuleta roho zingine saba zilizo chafu zaidi yake. Huingia na kuishi humo, na mtu huyo anakuwa na matatizo mengi kuliko mwanzo wakati roho chafu moja iliishi ndani yake. Ndivyo ilivyo kwa kizazi hiki cha watu wanaoishi leo.” Yesu alipokuwa akiongea na watu, mama yake na ndugu zake walikuwa nje. Walitaka kuongea naye. Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na wadogo zako wanakusubiri nje. Wanataka kuongea nawe.” Yesu akajibu, “Mama yangu ni nani? Ndugu zangu ni nani?” Kisha akanyoosha kidole kwa wafuasi wake na akasema, “Unaona! Watu hawa ni mama yangu na ndugu zangu. Kaka yangu, dada yangu na mama yangu halisi ni yule afanyaye yale Baba yangu wa mbinguni anataka.” Siku hiyo hiyo Yesu alitoka nje ya nyumba na kukaa kando ya ziwa. Kundi kubwa wakakusanyika kumzunguka. Hivyo akapanda mtumbwini na kuketi. Watu wote wakabaki ufukweni. Kisha Yesu akatumia simulizi kuwafundisha mambo mengi. Akawaambia simulizi hii: “Mkulima alitoka kwenda kupanda mbegu. Alipokuwa anatawanya mbegu, baadhi ziliangukia njiani. Ndege wakaja na kuzila zote. Mbegu zingine ziliangukia kwenye ardhi yenye mawe, ambako hakukuwa na udongo wa kutosha. Zikakua haraka pale, kwa sababu udongo haukuwa na kina. Lakini jua lilipowaka, likaichoma mimea. Mimea ikafa kwa sababu haikuwa na mizizi mirefu. Baadhi ya mbegu ziliangukia katikati ya miiba. Miiba ikakua na kusababisha mimea mizuri kuacha kukua. Lakini baadhi ya mbegu ziliangukia kwenye udongo wenye rutuba. Hapo zikakua na kuzaa nafaka. Baadhi ya mimea ikazaa nafaka mara mia zaidi, baadhi mara sitini na baadhi mara thelathini zaidi. Ninyi watu mnaoweza kunisikia, nisikilizeni!” Wafuasi wake wakamwendea Yesu na kumuuliza, “Kwa nini unatumia simulizi hizi kuwafundisha watu?” Yesu akawajibu, “Mungu amewapa ninyi ujuzi wa kuelewa siri za ufalme wa Mungu, lakini hajawapa watu hawa wengine ujuzi huu. Kisha akawaambia, ‘Zingatieni kwa makini kile mnachokisikia. Kwani jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa na kuzidi kuelewa. Kwa kuwa kila aliye na uelewa kidogo ataongezewa zaidi. Lakini wale wasiosikiliza kwa makini watapoteza hata ule uelewa mdogo walio nao.’ Ndiyo sababu ninatumia simulizi hizi kuwafundisha watu: Wanaona, lakini hakika hawaoni. Wanasikia, lakini hakika hawasikii au kuelewa. Hiyo inathibitisha alichosema nabii Isaya kuhusu wao kuwa kweli: ‘Ninyi watu mtasikia na kusikia, lakini hamtaelewa. Mtatazama na kutazama, lakini hakika hamtaona. Ndiyo, akili za watu hawa sasa zimefungwa. Wana masikio, lakini hawasikii vizuri. Wana macho, lakini wameyafumba. Iwapo akili zao zisingekuwa zimefungwa, wangeona kwa macho yao; wangesikia kwa masikio yao; Iwapo wangeelewa kwa akili zao. Kisha wangenigeukia na kuponywa.’ Bahati gani mliyonayo ninyi. Mnaelewa mnachokiona kwa macho yenu. Na mnaelewa mnachosikia kwa masikio yenu. Ninaweza kuwathibitishia, manabii na watakatifu wengi walitaka kuona mnayoyaona. Lakini hawakuyaona. Walitaka kusikia mnayosikia sasa. Lakini hawakuyasikia. Hivyo sikilizeni maana ya simulizi hiyo kuhusu mkulima: Vipi kuhusu mbegu zilizoangukia njiani? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho kuhusu ufalme wa Mungu lakini hawauelewi. Mwovu huja na kuyachukua yaliyopandwa katika mioyo yao. Na vipi kuhusu mbegu zilizoangukia kwenye udongo wenye mawe? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho haraka na kwa furaha huyapokea. Lakini hawaruhusu mafundisho kutawala maisha yao. Huyatunza kwa muda mfupi. Mara tatizo au mateso yanapokuja kwa sababu ya mafundisho waliyoyapokea, wanaacha kuyafuata. Na vipi kuhusu mbegu zilizoanguka katikati ya miiba? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho lakini huyaruhusu mahangaiko ya maisha na kutaka utajiri, hufanya mafundisho yasikue. Hivyo mafundisho hayazai mazao mazuri katika maisha yao. Lakini vipi kuhusu mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye rutuba? Hizo ni sawa na watu wanaosikia mafundisho na kuyaelewa. Hukua na kuzaa mazao mazuri, wakati mwingine mara mia, wakati mwingine mara sitini, na wakati mwingine mara thelathini zaidi.” Kisha Yesu akatumia simulizi nyingine kuwafundisha. Yesu akasema, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Usiku ule, kila mtu alipokuwa amelala, adui wa yule mtu akaja na kupanda magugu katikati ya ngano kisha akaondoka. Baadaye, ngano ikakua na vichwa vya nafaka vikaota juu ya mimea. Kisha mtumishi akayaona magugu. Watumwa wa mwenye shamba wakaja na akasema, ‘Bwana ulipanda mimea mizuri kwenye shamba lako. Magugu yametoka wapi?’ Yule mtu akajibu, ‘Adui alipanda magugu.’ Wale watumwa wakauliza, ‘Je, unataka twende na kung'oa magugu?’ Akajibu, ‘Hapana, kwa sababu mtakapokuwa mnang'oa magugu, mtaweza pia kung'oa ngano. Yaacheni magugu na ngano vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati wa mavuno nitawaambia wafanyakazi hivi: Kwanza, yakusanyeni magugu na kuyafunga pamoja ili myachome. Kisha kusanyeni ngano na kuileta ghalani mwangu.’” Kisha Yesu akawaambia watu simulizi nyingine: “Ufalme wa Mungu unafanana na mbegu ya mharadali ambayo mtu alipanda katika shamba lake. Ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote. Lakini unapokua, ni kubwa kuliko mimea yote ya bustanini. Unakuwa mti mkubwa unaotosha ndege kuja na kutengeneza viota kwenye matawi yake.” Kisha Yesu akawaambia simulizi nyingine: “Ufalme wa Mungu unafanana na chachu ambayo mwanamke huichanganya katika bakuli kubwa la unga ili atengeneze mkate. Chachu hufanya kinyunya chote kiumuke.” Yesu alitumia simulizi akasema mambo yote haya kwa watu. Daima alitumia simulizi kuwafundisha. Hii ilikuwa kuweka wazi maana halisi kama manabii walivyosema: “Nitazungumza kwa kutumia simulizi; Nitayasema mambo ambayo yamekuwa siri tangu ulimwengu ulipoumbwa.” Kisha Yesu akawaacha watu na kuingia katika nyumba. Wafuasi wake wakamwendea na akasema, “Tufafanulie maana ya simulizi kuhusu magugu ndani ya shamba.” Akajibu, “Mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba ni Mwana wa Adamu. Shamba ni ulimwengu. Mbegu nzuri ni watoto katika ufalme wa Mungu. Magugu ni watu wa Yule Mwovu. Na adui aliyepanda mbegu mbaya ni ibilisi. Mwisho wa nyakati ndiyo wakati wa mavuno. Wafanyakazi wanaokusanya ni malaika wa Mungu. Magugu hung'olewa na kuchomwa motoni. Itakuwa vivyo hivyo nyakati za mwisho. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watawatafuta watu wanaosababisha dhambi na wale wote watendao maovu. Malaika watawatoa watu hao katika ufalme wa Mungu. Watawatupia katika tanuru la moto. Huko watu watakuwa wakilia na kusaga meno kwa maumivu. Kisha wenye haki watang'aa kama jua. Watakuwa katika ufalme wa baba yao. Ninyi watu, mlio na masikio, sikilizeni! Ufalme wa Mungu unafanana na hazina iliyofichwa shambani. Siku moja mtu alipoiona aliificha tena; na kwa sababu alikuwa na furaha sana alikwenda kuuza kila kitu alichonacho na kulinunua shamba. Pia, ufalme wa Mungu unafanana na mchuuzi anayetafuta lulu safi. Siku moja alipoipata, alikwenda na akauza kila kitu alichokuwa nacho ili kuinunua. Pia, ufalme wa Mungu unafanana na nyavu kubwa iliyowekwa katika ziwa. Nyavu ile ikavua aina nyingi tofauti ya samaki. Ikajaa, hivyo wavuvi wakaivuta mpaka pwani. Wakakaa chini na kutoa samaki wote wazuri na kuwaweka kwenye kikapu. Kisha wakawatupa samaki wabaya. Itakuwa hivyo wakati wa mwisho. Malaika watakuja na kuwatenganisha waovu na watakatifu. Watawatupa waovu katika tanuru la moto. Huko watu watalia na kusaga meno yao kwa sababu ya maumivu.” Kisha Yesu akawauliza wafuasi wake, “Mnaelewa mambo yote haya?” Wakasema, “Ndiyo, tunaelewa.” Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivyo kila mwalimu wa sheria aliyejifunza kuhusu ufalme wa Mungu ana baadhi ya vitu vizuri vya kufundisha. Ni kama mmiliki wa nyumba, aliye na vitu vipya na vya zamani nyumbani mwake. Na huvitoa nje vipya na vya zamani.” Yesu alipomaliza kufundisha kwa simulizi hizi, aliondoka pale. Alikwenda katika mji wa kwao. Aliwafundisha watu katika sinagogi lao, nao walishangaa. Walisema, “Mtu huyu alipata wapi hekima na nguvu hii ya kutenda miujiza? Je, yeye si mwana wa seremala tunayemfahamu? Je, jina la mamaye si Mariamu na wadogo zake ni Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda? Na dada zake bado wanaishi hapa katika mji huu? Anawezaje kutenda mambo haya?” Hivyo wakawa na mashaka kumpokea. Lakini Yesu akawaambia, “Watu kila mahali huwaheshimu manabii, lakini katika mji wake au katika nyumba yake nabii hapati heshima yoyote.” Yesu hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu watu hawakumwamini. Katika wakati huo, Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia ambacho watu walikuwa wanasema kuhusu Yesu. Hivyo akawaambia watumishi wake, “Nadhani hakika mtu huyu ni Yohana Mbatizaji. Lazima amefufuka kutoka kwenye kifo, na ndiyo sababu anaweza kutenda miujiza hii.” Kabla ya wakati huu, Herode alimkamata Yohana. Akamfunga kwa minyororo na kumweka gerezani. Alimkamata Yohana kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, kaka yake Herode. Yohana alikuwa amemwambia, “Si sahihi kwako kumwoa Herodia.” Herode alitaka kumwua, lakini aliwaogopa watu. Waliamini kuwa Yohana alikuwa nabii. Siku ya kuzaliwa Herode, bintiye Herodia alicheza mbele yake na kundi lake. Herode alifurahishwa naye sana. Hivyo aliapa kuwa atampa kitu chochote atakachotaka. Herodia alimshawishi binti yake kitu cha kuomba. Hivyo bintiye akamwambia Herode, “Nipe hapa kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sahani kubwa.” Mfalme Herode alihuzunika sana. Lakini alikuwa ameahidi kumpa binti kitu chochote alichotaka. Na watu waliokuwa wakila pamoja na Herode walikuwa wamesikia ahadi yake. Hivyo Herode aliamuru kitu ambacho alikuwa ameomba apatiwe. Akawatuma wanaume gerezani, ambako walikikata kichwa cha Yohana. Na watu wakakileta kichwa cha Yohana kwenye sahani kubwa na kumpa yule msichana. Kisha yeye akakipeleka kichwa kwa mama yake, Herodia. Wafuasi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wa Yohana na kuuzika. Kisha wakaenda na kumwambia Yesu kilichotokea. Yesu aliposikia kilichotokea kwa Yohana, aliondoka kwa kutumia mtumbwi. Alikwenda peke yake mpaka mahali ambapo hakuna aliyekuwa akiishi. Lakini watu walisikia kuwa Yesu alikuwa ameondoka. Hivyo waliondoka katika miji na kumfuata. Walikwenda mahali alikokwenda kupitia nchi kavu. Yesu alipotoka katika mtumbwi, aliwaona watu wengi. Akawahurumia, na kuwaponya waliokuwa wagonjwa. Baadaye mchana huo, wafuasi walimwendea Yesu na kusema, “Hakuna anayeishi katika eneo hili. Na tayari muda umepita, hivyo waage watu ili waende katika miji na kujinunulia chakula.” Yesu akasema, “Watu hawahitaji kuondoka. Wapeni ninyi chakula wale.” Wafuasi wakajibu, “Lakini tuna mikate mitano na samaki wawili tu.” Yesu akasema, “Leteni kwangu mikate na samaki.” Kisha akawaambia watu waketi chini kwenye nyasi. Akaichukua mikate mitano na samaki wawili. Akatazama mbinguni na akamshukuru Mungu kwa ajili ya chakula. Kisha akaivunja mikate katika vipande, akawapa wafuasi wake nao wakawapa watu chakula. Kila mmoja alikula mpaka akashiba. Walipomaliza kula, wafuasi walijaza vikapu kumi na mbili vya vipande vilivyosalia. Walikuwepo wanaume 5,000, pamoja na wanawake na watoto waliokula. Mara baada ya hili Yesu akawaambia wafuasi wake wapande kwenye mtumbwi. Akawaambia waende upande mwingine wa ziwa. Aliwaambia angekuja baadaye, alikaa pale ili kuwaaga watu. Baada ya Yesu kuwaaga watu, alikwenda kwenye vilima peke yake kuomba. Ikawa jioni na alikuwa pale peke yake. Wakati huu mtumbwi ilikuwa mbali kutoka pwani. Kwa kuwa upepo ulikuwa unavuma kinyume na mtumbwi, mtumbwi ulikuwa unapata msukosuko kwa sababu ya mawimbi. Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi, wafuasi wa Yesu walikuwa bado ndani ya mtumbwi. Yesu akaenda kwao akitembea juu ya maji. Iliwatisha walipomwona anatembea juu ya maji. Wakapiga kelele kwa woga “Ni mzuka!” Lakini haraka Yesu akawaambia, “Msihofu! Ni mimi! Msiogope.” Petro akasema, “Bwana, ikiwa hakika ni wewe, niambie nije kwako juu ya maji.” Yesu akasema, “Njoo, Petro.” Kisha Petro akauacha mtumbwi na kutembea juu ya maji kumwelekea Yesu. Lakini Petro alipokuwa anatembea juu ya maji, aliyaona mawimbi na upepo. Aliogopa na kuanza kuzama katika maji. Akapiga kelele, “Bwana, niokoe!” Haraka Yesu akamshika Petro kwa mkono wake. Akasema, “Imani yako ni ndogo. Kwa nini ulisita?” Baada ya Petro na Yesu kuingia kwenye mtumbwi, upepo ukakoma. Kisha wafuasi wakamwabudu Yesu na kusema, “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.” Baada ya kuvuka ziwa, wakafika pwani katika eneo la Genesareti. Baadhi ya watu pale wakamwona Yesu na wakamtambua kuwa ni nani. Hivyo wakatuma ujumbe kwa watu wengine katika eneo lote kuwa Yesu amekuja. Watu wakawaleta wagonjwa wao wote kwake. Walimsihi Yesu awaruhusu waguse tu upindo wa vazi lake ili waponywe. Na wagonjwa wote waliogusa vazi lake waliponywa. Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria kutoka Yerusalemu walimjia Yesu na kumwuliza, “Kwa nini wafuasi wako hawatii desturi tulizorithi kutoka kwa viongozi wetu wakuu walioishi hapo zamani? Wafuasi wako hawanawi mikono kabla ya kula!” Yesu akajibu, “Na kwa nini mnakataa kutii amri ya Mungu ili muweze kuzifuata desturi zenu? Mungu alisema, ‘Ni lazima umtii baba na mama yako.’ Na Mungu alisema pia kuwa, ‘Kila anayemnenea vibaya mama au baba yake lazima auawe.’ Lakini mnafundisha kuwa mtu anaweza kumwambia baba au mama yake, ‘Nina kitu ninachoweza kukupa kukusaidia, Lakini sitakupa, bali nitampa Mungu.’ Mnawafundisha kutowatii baba zao. Hivyo mnafundisha kuwa si muhimu kufanya kile alichosema Mungu. Mnadhani ni muhimu kufuata mila na desturi zenu mlizonazo. Enyi wanafiki! Isaya alikuwa sahihi alipozungumza kwa niaba ya Mungu kuhusu ninyi aliposema: ‘Watu hawa wananiheshimu kwa maneno tu, lakini mimi si wa muhimu kwao. Ibada zao kwangu hazina maana. Wanafundisha kanuni za kibinadamu tu.’” Yesu akawaita watu. Akasema, “Sikieni na mwelewe nitakachosema. Si chakula kinachoingia mdomoni kinachomtia mtu unajisi, bali kile kinachomtoka mdomoni mwake.” Kisha wafuasi wakamjia na kumwuliza, “Unajua kuwa Mafarisayo wamekasirika kutokana na yale uliyosema?” Yesu akajibu, “Kila mti ambao haukupandwa na Baba yangu wa mbinguni utang'olewa. Kaeni mbali na Mafarisayo. Wanawaongoza watu, lakini ni sawa na wasiyeona wanaowaongoza wasiyeona wengine. Na kama asiyeona akimwongoza asiyeona mwingine, wote wawili wataangukia shimoni.” Petro akasema, “Tufafanulie yale uliyosema awali kuhusu kile kinachowatia watu najisi.” Yesu akasema, “Bado mna matatizo ya kuelewa? Hakika mnajua kuwa vyakula vyote vinavyoingia kinywani huenda tumboni. Kutoka huko hutoka nje ya mwili. Lakini mambo mabaya ambayo watu wanasema kwa vinywa vyao hutokana na mawazo yao. Na hayo ndiyo yanayoweza kumtia mtu unajisi. Mambo mabaya haya yote huanzia akilini: mawazo maovu, mauaji, uzinzi, uasherati, wizi, uongo, na matukano. Haya ndiyo mambo yanayowatia watu unajisi. Kula bila kunawa mikono hakuwezi kuwafanya watu wasikubaliwe na Mungu.” Kutoka pale, Yesu alikwenda maeneo ya Tiro na Sidoni. Mwanamke Mkanaani kutoka eneo hilo akatokea na kuanza kupaza sauti, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali nisaidie! Binti yangu ana pepo ndani yake, na anateseka sana.” Lakini Yesu hakumjibu. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea Yesu na kumwambia, “Mwambie aondoke, anaendelea kupaza sauti na hatatuacha.” Yesu akajibu, “Mungu alinituma niwasaidie kondoo wa Mungu waliopotea, watu wa Israeli.” Ndipo mwanamke alikuja mahali alipokuwa Yesu na kuinama mbele yake. Akasema, “Bwana, nisaidie!” Akamjibu kwa kumwambia, “Si sahihi kuwapa mbwa mkate wa watoto.” Mwanamke akasema, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula vipande vya chakula vinavyoanguka kutoka kwenye meza za mabwana zao.” Kisha Yesu akamjibu, “Mwanamke, una imani kuu! Utapata ulichoomba.” Wakati huo huo binti wa yule mwanamke akaponywa. Kisha Yesu akatoka pale na kwenda pwani ya Ziwa Galilaya. Alipanda vilima na akaketi chini. Kundi kubwa la watu likamwendea. Walileta watu wengine wengi waliokuwa wagonjwa na kuwaweka mbele yake. Walikuwepo watu wasioweza kutembea, wasiyeona, walemavu wa miguu, wasiyesikia na wengine wengi. Watu walishangaa walipoona kuwa waliokuwa wasiyesema walianza kusema, walemavu wa miguu waliponywa, waliokuwa hawawezi kutembea waliweza kutembea, wasiyeona waliweza kuona. Kila mtu alimshukuru Mungu wa Israeli kwa hili. Kisha Yesu akawaita wafuasi wake na kuwaambia, “Ninawaonea huruma watu hawa. Wamekuwa pamoja nami kwa siku tatu, na sasa hawana chakula. Sitaki niwaache waende wakiwa na njaa. Wanaweza kuzimia njiani wanaporudi nyumbani.” Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha watu wote hawa? Tuko nyikani mbali ni miji.” Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?” Wakamjibu, “Tuna mikate saba na samaki wadogo wachache.” Yesu akawaambia watu waketi chini. Akaichukua mikate saba na samaki. Akamshukuru Mungu kwa sababu ya chakula. Akaigawa vipande vipande, akawapa wafuasi wake na wafuasi wakawapa watu chakula. Watu wote walikula mpaka wakashiba. Baada ya hili, wafuasi walijaza vikapu saba kwa vipande vya chakula vilivyosalia ambavyo havikuliwa. Walikuwepo wanaume 4,000 pale waliokula. Walikuwepo pia wanawake na watoto. Baada ya wote kula, Yesu akawaambia watu wanaweza kwenda nyumbani. Alipanda mashua na kwenda eneo la Magadani. Mafarisayo na Masadukayo walimjia Yesu. Walitaka kumjaribu, kwa hiyo wakamwomba awaoneshe muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Yesu akawajibu, “Ninyi watu mnapoona jua limezama, mnajua hali ya hewa itakavyokuwa. Anga ikiwa nyekundu, mnasema tutakuwa na hali ya hewa nzuri. Na asubuhi, ikiwa anga ni nyeusi na nyekundu, mnasema mvua itanyesha. Hizi ni ishara za hali ya hewa. Mnaziona ishara hizi angani na mnajua zinamaanisha nini. Kwa namna hiyo hiyo, mnaona mambo yanayotokea sasa. Hizi ni ishara pia, lakini hamwelewi maana yake. Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu na si waaminifu kwa Mungu. Ndiyo sababu kabla ya kuamini mnataka kuona muujiza. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia kitu cho chote. Yona ndiyo ishara pekee mtakayopewa.” Kisha Yesu akaondoka mahali pale. Yesu na wafuasi wake wakasafiri kwa kukatisha ziwa. Lakini wafuasi wakasahau kubeba mikate. Yesu akawaambia, “Mwe waangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” Wafuasi wakajadiliana maana ya hili. Wakasema, “Amesema hivi kwa sababu tumesahau kubeba mikate?” Yesu alipotambua kuwa wanajadiliana hili, akawauliza, “Kwa nini mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Imani yenu ni ndogo. Bado hamwelewi? Mnakumbuka mikate mitano waliyokula watu 5,000 na vikapu vingi mlivyojaza mikate iliyosalia? Na mnakumbuka mikate saba waliyokula watu 4,000 na vikapu vingi mlivyojaza wakati ule? Hivyo inakuwaje mnadhani kuwa mimi ninajali sana kuhusu mikate? Ninawaambia muwe waangalifu na mjilinde dhidi ya chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” Ndipo wafuasi wakaelewa Yesu alimaanisha nini. Hakuwa akiwaambia wajilinde na chachu inayotumika katika mikate bali wajilinde na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo. Yesu alikwenda eneo la Kaisaria Filipi na akawauliza wafuasi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?” Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji. Wengine wanasema wewe ni Eliya. Na wengine wanasema wewe ni Yeremia au mmoja wa manabii.” Kisha Yesu akawauliza, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?” Simoni Petro akajibu, “Wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu aliye hai.” Yesu akajibu, “Umebarikiwa, Simoni mwana wa Yona. Hakuna aliyekufundisha hilo ila Baba yangu wa mbinguni ndiye amekuonesha mimi ni nani. Hivyo ninakwambia, Wewe ni Petro. Na nitalijenga kanisa langu kwenye mwamba huu. Nguvu ya mauti haitaweza kulishinda kanisa langu. Nitawapa funguo za Ufalme wa Mungu. Mnapohukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Mnapotamka msamaha hapa duniani, msamaha huo utakuwa msamaha wa Mungu.” Kisha Yesu akawaonya wafuasi wake wasimwambie mtu yeyote kuwa yeye ndiye Masihi. Kuanzia wakati huo Yesu alianza kuwaambia wafuasi wake kuwa ni lazima aende Yerusalemu. Alifafanua kuwa Viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria watamfanya apate mateso kwa mambo mengi. Na aliwaambia wafuasi wake kuwa lazima auawe. Na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. Petro akamchukua Yesu na kwenda naye faragha mbali na wafuasi wengine. Akaanza kumkosoa Yesu kwa akasema, “Mungu akuepushe mbali na mateso hayo, Bwana! Hilo halitakutokea!” Ndipo Yesu akamwambia Petro, “Ondoka kwangu, Shetani! Hunisaidii! Hujali mambo ya Mungu. Unajali mambo ambayo wanadamu wanadhani ni ya muhimu.” Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Ikiwa yeyote miongoni mwenu anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima aache kujiwazia yeye mwenyewe na mahitaji yake. Ni lazima awe radhi kuubeba msalaba aliopewa na kunifuata mimi. Yeyote kati yenu anayetaka kuokoa uhai wake, ataupoteza. Lakini ninyi mlioyaacha maisha yenu kwa ajili yangu mtaupata uzima wa kweli. Haina maana kwenu ninyi kuupata ulimwengu wote, ikiwa ninyi wenyewe mtapotea. Mtu atalipa nini ili kuyapata tena maisha yake baada ya kuyapoteza? Mimi, Mwana wa Adamu, nitarudi katika utukufu wa Baba yangu pamoja na Malaika. Na nitamlipa kila mtu kutokana na matendo yake. Niaminini ninaposema wapo watu waliopo hapa watakaoishi mpaka watakaponiona nikija kama Mwana wa Adamu kutawala kama mfalme.” Siku sita baadaye, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo na akapanda nao kwenye mlima mrefu. Walikuwa peke yao huko. Wafuasi wake hawa walipokuwa wakimwangalia, Yesu alibadilika. Uso wake ukawa angavu kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama mwanga. Ndipo wanaume wawili waliozungumza naye wakaonekana wakiwa pamoja naye. Walikuwa Musa na Eliya. Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tuko hapa. Ukitaka, nitajenga vibanda vitatu, kimoja kwa ajili ya heshima yako, kingine kwa ajili ya heshima ya Musa na kingine kwa ajili ya heshima ya Eliya.” Petro alipokuwa akizungumza, wingu jeupe liliwafunika. Sauti ikatoka katika wingu na akasema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda, ninafurahishwa naye. Mtiini yeye!” Wafuasi waliokuwa na Yesu walipoisikia sauti hii waliogopa sana na wakaanguka chini. Lakini Yesu akawaendea na kuwagusa. Akasema, “simameni, msiogope.” Wafuasi wakatazama juu, wakaona kuwa Yesu yuko peke yake. Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanateremka kutoka mlimani, akawaamuru akisema: “Msimwambie mtu yeyote yale mliyoyaona mlimani. Subirini mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu. Ndipo mtaweza kuwaambia watu juu ya kile mlichokiona.” Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Kwa nini walimu wa sheria wanasema ni lazima Eliya aje kabla ya Masihi kuja?” Yesu akajibu, “Wako sahihi kusema ni lazima Eliya aje, na ni kweli kuwa Eliya ataweka mambo yote kama yanavyopaswa kuwa. Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja. Watu hawakumjua yeye ni nani, na walimtendea vibaya, wakafanya kama walivyotaka. Ndivyo itakavyokuwa hata kwa Mwana wa Adamu. Watu hao punde tu watamletea mateso Mwana wa Adamu.” Ndipo wafuasi wakaelewa kuwa Yesu aliposema kuhusu Eliya, alikuwa anazungumza juu ya Yohana Mbatizaji. Yesu na wafuasi walirudi kwa watu. Mtu mmoja akamjia Yesu na kuinama mbele zake. Akasema, “Bwana, umwonee huruma mwanangu. Anateswa sana na kifafa alichonacho. Anaangukia kwenye moto au maji mara kwa mara. Nilimleta kwa wafuasi wako, lakini wameshindwa kumponya.” Yesu akajibu, “Ninyi watu mnaoishi katika nyakati hizi cha kizazi kisicho na imani. Maisha yenu ni mabaya sana! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kijana hapa.” Yesu akamwamuru pepo aliye ndani ya kijana, na pepo akamtoka na yule kijana akapona. Kisha wafuasi wakamjia Yesu wakiwa peke yao. Wakasema, “Tulijaribu kumtoa pepo kwa kijana, lakini tulishindwa. Kwa nini tulishindwa kumtoa pepo?” Yesu akajibu, “Mlishindwa kumtoa pepo kwa sababu imani yenu ni ndogo sana. Niaminini ninapowaambia, imani yenu ikiwa na ukubwa wa mbegu ya haradali mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ondoka hapa na uende kule,’ nao utaondoka. Nanyi mtaweza kufanya jambo lolote.” *** Baadaye, wafuasi walipokusanyika pamoja Galilaya, Yesu aliwaambia, “Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwenye mamlaka ya watu wengine, watakaomwua. Lakini atafufuliwa kutoka kwa wafu siku ya tatu.” Wafuasi waliposikia kuwa Yesu angeuawa walihuzunika sana. Yesu na wafuasi wake walikwenda Kapernaumu. Walipofika huko watu waliokuwa wakikusanya ushuru wa Hekalu wakamwendea Petro na kumwuliza, “Je, mwalimu wenu hulipa kodi ya Hekalu?” Petro akajibu, “Ndiyo, hulipa.” Petro akaingia katika nyumba alimokuwa Yesu. Kabla Petro hajazungumza jambo lolote, Yesu akamwambia, “Wafalme wa dunia huchukua kila aina ya kodi kutoka kwa watu. Lakini ni akina nani ambao hutoa kodi? Je, ni jamaa wa familia ya mfalme? Au watu wengine ndiyo hulipa kodi? Unadhani ni akina nani?” Petro akajibu, “Watu wengine ndiyo hulipa kodi.” Yesu akasema, “Basi wana wa mfalme hawapaswi kulipa kodi. Lakini kwa kuwa hatutaki kuwaudhi watoza ushuru hawa, basi fanya hivi: Nenda ziwani na uvue samaki. Utakapomkamata samaki wa kwanza, mfungue kinywa chake. Ndani ya kinywa chake utaona sarafu nne za drakma mdomoni mwake. Ichukue sarafu hiyo mpe mtoza ushuru. Hiyo itakuwa kodi kwa ajili yangu mimi na wewe.” Wakati huo huo wanafunzi wake wakamjia Yesu na kuuliza, “Nani ni mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu?” Yesu akamwita mtoto mdogo, akamsimamisha mbele yao. Kisha akasema, “Ukweli ni huu, ni lazima mbadilike katika namna mnavyofikiri na muwe kama mtoto mdogo. Msipofanya hivi hamtaingia katika ufalme wa Mungu. Aliye mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu ni yule anayejinyenyekeza kama mtoto huyu. Unapomkubali mtoto mdogo kama huyu kama aliye wangu, unanikubali mimi. Ikiwa mmoja wa watoto hawa wadogo ananiamini, na mtu yeyote akasababisha mtoto huyo kutenda dhambi, ole wake mtu huyo. Ingekuwa bora mtu huyo kufungiwa jiwe la kusagia shingoni mwake na kuzamishwa katika kina kirefu baharini. Nawasikitikia watu wa ulimwengu kwa sababu ya mambo yanayofanya watu watende dhambi. Mambo haya lazima yatokee, lakini ole wake mtu yeyote anayeyafanya yatokee. Mkono au mguu wako ukikufanya utende dhambi, ukate na uutupe. Ni bora ukapoteza kiungo kimoja cha mwili wako na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na mikono au miguu miwili na ukatupwa katika moto wa milele. Jicho lako likikufanya utende dhambi, ling'oe na ulitupe. Ni bora kwako kuwa na jicho moja tu na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na macho mawili na ukatupwa katika moto wa Jehanamu. Iweni waangalifu, msidhani kuwa watoto hawa wadogo si wa muhimu. Ninawaambia kuwa watoto hawa wana malaika mbinguni. Na hao malaika daima wako pamoja na Baba yangu mbinguni. *** Mtu akiwa na kondoo 100, lakini mmoja wa kondoo akapotea, atafanya nini? Atawaacha kondoo wengine 99 kwenye kilima na kwenda kumtafuta mmoja aliyepotea. Sawa? Na akimpata kondoo aliyepotea, atafurahi kwa sababu ya kondoo huyo mmoja kuliko kondoo wengine 99 ambao hawakupotea. Ninaweza kuwathibitishia, Kwa namna hiyo hiyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi mmoja wa watoto hawa wadogo apotee. Ikiwa mmoja wa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akifanya kosa kwako, umwendee na umwambie kile alichokukosea. Ufanye hivi mnapokuwa ninyi wawili tu. Ikiwa mtu huyo atakusikiliza, basi umemsaidia na umfanye kuwa kaka ama dada yako tena. Lakini ikiwa mtu huyo atakataa kukusikiliza, mrudie ukiwa pamoja na ndugu wengine wawili waaminio. Ndipo watakuwepo watu wawili au watatu watakaoweza kueleza kile kilichotokea. Ikiwa mtu aliyetenda dhambi atakataa kuwasikiliza, ndipo uliambie kanisa. Na akikataa kulisikiliza kanisa, mchukulie kama ambavyo ungemchukulia mtu asiyemfahamu Mungu au mtoza ushuru. Ninawahakikishia kuwa mnapotoa hukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Na mnapotoa msamaha, nao utakuwa msamaha wa Mungu. Kwa namna nyingine, ikiwa watu wawili waliopo duniani watakubaliana kwa kila wanachokiombea, Baba yangu wa mbinguni atatenda kile wanachokiomba. Ndiyo, ikiwa watu wawili au watatu wanaoniamini watakusanyika pamoja, mimi nitakuwa pamoja nao.” Kisha Petro akamwendea Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu akiendelea kunikosea, ninapaswa kumsamehe anaponikosea mara ngapi? Mara saba?” Yesu akamjibu, “Ninakwambia, ni lazima umsamehe zaidi ya mara saba. Ni lazima uendelee kumsamehe hata kama atakukosea saba mara sabini. Ninawaambia kwa sababu ufalme wa Mungu unafanana na mfalme aliyetaka kupata taarifa kutoka kwa watumishi wake. Mtumishi aliyekuwa anadaiwa na mfalme tani 300 za fedha aliletwa kwake. Hakuwa na fedha za kutosha kulipa deni lake. Hivyo mfalme aliamuru kila kitu anachomiliki mtumishi yule kiuzwe ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake. Lakini mtumishi alipiga magoti na kumsihi mfalme akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’ Mfalme alimhurumia. Hivyo akamsamehe yule mtumishi deni lote na akamwacha aende akiwa huru. Lakini mtumishi huyo alipoondoka, alimwona mtumishi mwingine aliyekuwa anamdai sarafu mia za fedha. Akamkaba shingo yake na akasema, ‘Nilipe pesa ninayokudai!’ Mtumishi anayedaiwa akapiga magoti na kumsihi akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’ Lakini mtumishi wa kwanza alikataa kumvumilia. Alimwambia hakimu kuwa alikuwa anamdai pesa, na mtumishi yule alitupwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa deni lake. Watumishi wengine walipoona hili, walimhurumia mtumishi aliyefungwa gerezani. Hivyo walienda na kumwambia mfalme kila kitu kilichotokea. Ndipo mfalme alimwita msimamizi wa kwanza na kumwambia, ‘Wewe ni mbaya sana! Ulinisihi nikusamehe deni lako, na nilikuacha ukaondoka bila kulipa kitu chochote! Hivyo ulipaswa kumpa mtu yule mwingine anayetumika pamoja nawe rehema ile ile niliyokupa mimi.’ Mfalme alikasirika sana. Hivyo alifungwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa kila kitu anachodaiwa. Mfalme huyu alifanya kama ambavyo Baba yangu wa mbinguni atawafanyia ninyi. Ni lazima umsamehe ndugu au dada yako kwa moyo wako wote, usipofanya hivyo, Baba yangu wa mbinguni hatakusamehe wewe.” Yesu alipomaliza kuzungumza haya yote, aliondoka Galilaya. Alikwenda maeneo ya Yuda ng'ambo ya Mto Yordani. Watu wengi walimfuata na akaponya wagonjwa wengi huko. Baadhi ya Mafarisayo wakamjia Yesu. Walitaka aseme jambo fulani lisilo sahihi. Wakamwuliza, “Je, ni sahihi kwa mume kumtaliki mke wake kutokana na sababu yoyote ile kama anavyotaka?” Yesu akajibu, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko: Mungu alipoumba ulimwengu, ‘aliumba watu wa jinsi ya kiume na wa jinsi ya kike.’ Na Mungu alisema, ‘Hii ndiyo sababu mwanaume atawaacha baba na mama yake na kuungana na mke wake. Na hao watu wawili watakuwa mmoja.’ Hivyo wao si wawili tena, bali mmoja. Ni Mungu aliowaunganisha pamoja, hivyo mtu yeyote asiwatenganishe.” Mafarisayo wakauliza, “Sasa kwa nini Musa alitoa amri ya kumruhusu mwanaume kumtaliki mke wake kwa kuandika hati ya talaka?” Yesu akajibu, “Musa aliwaruhusu kuwataliki wake zenu kwa sababu mlikataa kupokea mafundisho ya Mungu. Lakini talaka haikuruhusiwa hapo mwanzo. Ninawaambia kuwa, kila anayemtaliki mke wake, isipokuwa kutokana na uzinzi, na akamwoa mwanamke mwingine, anazini.” Wafuasi wakamwambia Yesu, “Ikiwa hiyo ndiyo sababu pekee ambayo mtu anaruhusiwa kumtaliki mke wake, ni bora kutooa.” Akajibu, “Tamko hili ni la kweli kwa baadhi ya watu, lakini si kwa kila mtu. Bali ni kwa wale tu waliopewa karama hii. Kuna sababu tofauti kwa nini baadhi ya wanaume hawaoi. Wengine wamezaliwa wakiwa hawana uwezo wa kuzaa watoto, wengine walifanywa hivyo katika maisha yao ya baadaye. Na wengine walichagua kutokuoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Hili liko hivyo kwa kila anayeweza kulikubali.” Ndipo watu wakawaleta watoto wao wadogo kwa Yesu ili awabariki na kuwaombea. Wafuasi wake walipoliona hili, waliwakataza watu wasiwalete watoto kwa Yesu. Lakini Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto hawa wadogo.” Baada ya Yesu kuwabariki watoto, aliondoka huko. Mtu mmoja alimwendea Yesu na kumwuliza, “Mwalimu, nifanye jambo gani lililo jema ili niweze kuupata uzima wa milele?” Yesu akajibu, “Kwa nini unaniuliza kuhusu jambo gani lililo jema? Mungu pekee yake ndiye mwema. Lakini ikiwa unataka kuupata uzima wa milele, zitii amri.” Yule mtu akauliza, “Amri zipi?” Yesu akajibu, “‘Usiue, usizini, usiibe, usiseme uongo, mheshimu baba na mama yako,’ na ‘mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’” Yule kijana akasema, “Ninazitii amri hizi zote. Nifanye nini zaidi?” Yesu akajibu, “Ikiwa unataka kuwa mkamilifu, nenda ukauze kila kitu unachomiliki. Uwape pesa maskini na utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha njoo unifuate!” Lakini kijana aliposikia Yesu anamwambia kuhusu kugawa pesa yake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa kuwa alikuwa tajiri sana. Hivyo aliondoka. Ndipo Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Ukweli ni huu, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Ndiyo, ninawaambia, ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Wafuasi waliposikia hili walishangaa. Wakauliza, “Sasa ni nani ataweza kuokolewa?” Yesu akawatazama na kuwaambia, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, Lakini yote yanawezekana kwa Mungu.” Petro akamwambia, “Tuliacha kila kitu tulichonacho na kukufuata wewe. Tutapata nini?” Yesu akawaambia, “Wakati wa ulimwengu mpya utakapofika, Mwana wa Adamu ataketi kwenye kiti chake cha enzi, kikuu na chenye utukufu mwingi. Na ninaweza kuwaahidi kuwa ninyi mnaonifuata mtaketi kwenye viti kumi na viwili vya enzi, na mtayahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. Kila aliyeacha nyumba, ndugu, dada, baba, mama, watoto au shamba na akanifuata atapata zaidi ya yale aliyoacha. Na atapata uzima wa milele. Watu wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo. Na walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo. Ufalme wa Mungu umefanana na mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Asubuhi mmoja akatoka kwenda kuajiri watu ili walime katika shamba lake la mizabibu. Alikubaliana nao kuwa atawalipa sarafu moja ya fedha ikiwa watafanya kazi siku ile. Kisha akawapeleka kwenye shamba la mizabibu kulima. Ilipofika saa tatu asubuhi mtu huyo alitoka na kwenda sokoni ambako aliwaona baadhi ya watu wamesimama na hawafanyi kazi yo yote. Akawaambia, ‘Ikiwa mtakwenda kufanya kazi shambani kwangu, nitawalipa kutokana na kazi yenu.’ Hivyo walikwenda kufanya kazi kwenye shamba lake la mizabibu. Ilipofika saa sita mchana na saa tisa alasiri alitoka tena. Na nyakati zote mbili aliwaajiri watu wengine waende kufanya kazi shambani mwake. Ilipofika saa kumi na moja alikwenda sokoni tena. Akawaona watu wengine wamesimama pale. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa siku nzima na hamfanyi kazi?’ Wakasema, ‘Hakuna aliyetupa kazi.’ Mwenye shamba akawaambia, ‘Basi mnaweza kwenda kufanya kazi katika shamba langu la mizabibu.’ Mwishoni mwa siku, mwenye shamba akamwambia msimamizi wa wafanyakazi wote, ‘Waite wafanyakazi na uwalipe wote. Anza kwa kulipa watu niliowaajiri mwishoni, na malizia kwa wale niliowaajiri mwanzoni.’ Wafanyakazi walioajiriwa saa kumi na moja jioni walipata malipo yao. Kila mfanyakazi alipata sarafu moja ya fedha. Ndipo wafanyakazi walioajiriwa kwanza wakaja kupokea malipo yao. Walidhani wangelipwa zaidi ya wengine. Lakini kila mmoja wao alipokea sarafu moja ya fedha. Walipopata sarafu ya fedha, walimlalamikia mmiliki wa shamba. Walisema, ‘Watu hao walioajiriwa mwishoni wamefanya kazi saa moja tu. Lakini umewalipa sawa na sisi. Na tumefanya kazi siku nzima kwenye jua kali.’ Lakini mmiliki wa shamba akamwambia mmoja wao, ‘Rafiki, nimekulipa kama tulivyopatana, ulikubali kufanya kazi kwa malipo ya sarafu moja ya fedha. Sawa? Hivyo chukua malipo yako na uende. Ninataka kumlipa mtu niliyemwajiri mwishoni sawa na kiasi nilichokulipa. Ninaweza kufanya chochote ninachotaka na pesa yangu. Wewe unao wivu na unataka kuwadhuru wengine kwa kuwa mimi ni mkarimu?’ Hivyo walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo. Na walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo.” Yesu alikuwa anakwenda Yerusalemu akiwa na wafuasi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakitembea, aliwakusanya pamoja wafuasi hao na kuzungumza nao kwa faragha. Akawaambia, “Tunakwenda Yerusalemu. Mwana wa Adamu atatolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, nao watasema ni lazima auawe. Watamkabidhi wa wageni, watakaomcheka na kumpiga kwa mijeledi, kisha watamwua kwenye msalaba. Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, atafufuliwa kutoka kwa wafu.” Ndipo mke wa Zebedayo akamjia Yesu akiwa na wanaye. Akainama mbele ya Yesu na akamwomba amtendee kitu. Yesu akasema, “Unataka nini?” Akasema, “Niahidi kuwa mmoja wa wanangu atakaa upande wa kuume na mwingine wa kushoto katika ufalme wako.” Hivyo Yesu akawaambia wana wa Zebedayo, “Hamwelewi mnachokiomba. Mnaweza kukinywea kikombe ambacho ni lazima nikinywee?” Wana wa Zebedayo wakajibu, “Ndiyo tunaweza!” Yesu akawaambia, “Ni kweli kuwa mtakinywea kikombe nitakachokinywea. Lakini si mimi wa kuwaambia ni nani ataketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto. Baba yangu amekwisha amua ni nani ataketi kuume au kushoto kwangu. Amekwisha andaa nafasi hizo kwa ajili yao.” Wafuasi wengine kumi waliposikia hili walikasirika kwa ajili ya wale ndugu wawili. Hivyo Yesu akawaita pamoja, akawaambia, “Mnajua kuwa watawala wa watu wasio Wayahudi wanapenda kuonesha nguvu yao kwa watu. Na viongozi wao muhimu wanapenda kutumia mamlaka yao yote juu ya watu. Lakini isiwe hivyo miongoni mwenu. Kila anayetaka kuwa kiongozi wenu lazima awe mtumishi wenu. Kila anayetaka kuwa wa kwanza ni lazima awatumikie ninyi nyote kama mtumwa. Fanyeni kama nilivyofanya: Mwana wa Adamu hakuja ili atumikiwe na watu. Alikuja ili awatumikie wengine na kutoa maisha yake ili kuwaokoa watu wengi.” Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wanaondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata. Walikuwepo wasiyeona wawili wamekaa kando ya njia. Waliposikia kuwa Yesu anapita pale walipaza sauti wakasema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali tusaidie!” Watu waliwakemea wale wasiyeona, wakawaambia wanyamaze. Lakini waliendelea kupaza sauti zao zaidi na zaidi, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali tusaidie!” Yesu alisimama na kuwaambia, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakajibu, “Bwana, tunataka tuweze kuona.” Yesu aliwahurumia wale wasiyeona. Akayagusa macho yao, na mara hiyo hiyo wakaanza kuona. Wakawa wafuasi wa Yesu. Yesu na wafuasi wake walipokaribia Yerusalemu, walisimama Bethfage kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Wakiwa hapo Yesu aliwatuma wafuasi wake wawili mjini. Aliwaambia, “Nendeni kwenye mji mtakaoweza kuuona huko. Mtakapoingia katika mji huo, mtamwona punda na mwanapunda wake. Wafungueni wote wawili, kisha waleteni kwangu. Mtu yeyote akiwauliza kwa nini mnawachukua punda, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji. Atawarudisha mapema.’” Hili lilitimiza maneno yaliyosemwa na nabii: “Waambie watu wa Sayuni, ‘Mfalme wako anakuja sasa. Ni mnyenyekevu na amempanda punda. Na amempanda mwana punda dume tena safi.’” Wafuasi walikwenda na kufanya yale walioambiwa na Yesu. Waliwaleta kwake punda jike na mwanapunda. Waliwafunika punda kwa nguo zao na Yesu akaketi juu yao. Akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, watu wengi walitandaza mavazi yao barabarani kwa ajili Yake. Wengine walikata matawi ya miti na kuyatandaza barabarani ili kumkaribisha. Wengine walimtangulia Yesu, na wengine walikuwa nyuma yake. Wote walipaza sauti wakisema: “Msifuni Mwana wa Daudi! ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana!’ Msifuni Mungu wa mbinguni!” Kisha Yesu aliingia Yerusalemu. Watu wote mjini wakataharuki. Wakauliza, “Mtu huyu ni nani?” Kundi la watu waliomfuata Yesu wakajibu, “Huyu ni Yesu. Ni nabii kutoka katika mji wa Nazareti ulio Galilaya.” Yesu alipoingia katika eneo la Hekalu, aliwatoa nje wote waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Alizipindua meza za watu waliokuwa wanabadilishana pesa. Na alipindua viti vya watu waliokuwa wanauza njiwa. Yesu aliwaambia, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litaitwa nyumba ya sala.’ Lakini mmelibadilisha na kuwa ‘maficho ya wezi’. ” Baadhi ya watu waliokuwa wasiyeona na walemavu wa miguu walimjia Yesu alipokuwa eneo la Hekalu, naye aliwaponya. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria waliona mambo ya ajabu aliyokuwa anatenda. Na waliona watoto walivyokuwa wanamsifu wakisema, “Sifa kwa Mwana wa Daudi.” Mambo haya yote yaliwakasirisha makuhani na walimu wa sheria. Wakamwuliza Yesu, “Unasikia wanayosema watoto hawa?” Akajibu, “Ndiyo. Maandiko yanasema, ‘Umewafundisha watoto wadogo na watoto wanyonyao kusifu.’ Hamjasoma Maandiko haya?” Kisha Yesu akawaacha na akaenda katika mji wa Bethania akalala huko. Mapema asubuhi iliyofuata, Yesu alikuwa anarudi mjini Yerusalemu naye alikuwa na njaa. Aliuona mtini karibu na njia na akaenda kuchuma tini kwenye mti huo. Yalikuwepo maua tu. Hivyo Yesu akauambia mti ule, “Hautazaa matunda tena!” Mtini ukakauka na kufa hapo hapo. Wafuasi wake walipoona hili, walishangaa sana. Wakauliza, “Imekuwaje mtini ukakauka na kufa haraka hivyo?” Yesu akajibu, “Ukweli ni kuwa, mkiwa na imani na msiwe na mashaka, mtaweza kufanya kama nilivyofanya kwa mti huu. Na mtaweza kufanya zaidi ya haya. Mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ujitupe baharini.’ Na ikiwa una imani, litafanyika. Mkiamini, mtapokea kila mnachoomba.” Yesu aliingia katika eneo la Hekalu na akaanza kufundisha humo. Viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wakamjia. Wakasema, “Tuambie! Una mamlaka gani ya kufanya mambo haya unayofanya? Na nani amekupa mamlaka hii?” Yesu akajibu, “Nitawauliza swali pia. Mkinijibu, ndipo nitawaambia nina mamlaka gani ya kufanya mambo haya. Niambieni: Yohana alipowabatiza watu, mamlaka yake ilitoka kwa Mungu au kwa wanadamu?” Makuhani na viongozi wa Kiyahudi wakajadiliana kuhusu swali la Yesu, wakasemezana, “Tukisema, ‘Ubatizo wa Yohana ulitoka kwa Mungu,’ atasema, ‘Sasa kwa nini hamkumwamini Yohana?’ Lakini hatuwezi kusema ubatizo wa Yohana ulitoka kwa watu wengine. Tunawaogopa watu, kwa sababu wote wanaamini kuwa Yohana alikuwa nabii.” Hivyo wakamwambia Yesu, “Hatujui jibu.” Yesu akasema, “Basi hata mimi siwaambii aliyenipa mamlaka ya kufanya mambo haya.” “Niambieni mnafikiri nini kuhusu hili: Alikuwepo mtu mwenye wana wawili. Alimwendea mwanaye wa kwanza na kumwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’ Mwanaye akasema, ‘Siendi.’ Lakini baadaye akabadili uamuzi wake na akaenda. Kisha baba akamwendea mwanaye mwingine na kumwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’ Akajibu, ‘Sawa baba, nitakwenda kufanya kazi.’ Lakini hakwenda. Ni yupi kati ya wana hawa wawili alimtii baba yake?” Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ni mwana wa kwanza.” Yesu akawaambia, “Ukweli ni huu, ninyi ni wabaya kuliko watoza ushuru na makahaba. Ukweli ni kuwa hao wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu. Yohana alikuja akiwaonesha njia sahihi ya kuishi, na hamkumwamini. Lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini Yohana. Mliona yaliyotokea, lakini hamkubadilika na mlikataa kumwamini. Sikilizeni simulizi hii: Alikuwepo mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Alijenga uzio kuzunguka shamba lile la mizabibu na akachimba shimo kwa ajili ya kukamulia zabibu. Kisha akajenga mnara wa lindo. Akalikodisha shamba kwa wakulima kisha akasafiri. Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, akawatuma watumishi wake waende kwa wakulima ili apate gawio lake la zabibu. Lakini wakulima waliwakamata wale watumishi na kumpiga mmoja wao. Wakamwua mwingine na wa tatu wakampiga kwa mawe mpaka akafa. Hivyo mwenye shamba akawatuma baadhi ya watumishi wengine wengi zaidi ya aliowatuma hapo kwanza. Lakini wakulima wakawatendea kama walivyowatendea watumishi wa kwanza. Hivyo mwenye shamba akaamua kumtuma mwanaye kwa wakulima. Alisema, ‘Wakulima watamheshimu mwanangu.’ Lakini wakulima walipomwona mwanaye, wakaambizana, ‘Huyu ni mwana wa mwenye shamba. Shamba hili litakuwa lake. Tukimwua, shamba la mizabibu litakuwa letu.’ Hivyo wakulima wakamchukua mwana wa mwenye shamba, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu na kumwua. Hivyo mmiliki wa shamba la mizabibu atawafanya nini wakulima hawa atakaporudi?” Makuhani wa Kiyahudi na viongozi wakasema, “Kwa hakika atawaua watu hao waovu. Kisha atawakodishia wakulima wengine shamba hilo, watakaompa gawio la mazao yake wakati wa mavuno.” Yesu akawaambia, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko: ‘Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni. Bwana amefanya hivi, na ni ajabu kubwa kwetu kuliona.’ Hivyo ninawaambia kuwa, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na watapewa watu wanaofanya mambo anayoyataka Mungu katika ufalme wake. Kila aangukaye kwenye jiwe hili atavunjika na litamsaga kila linayemwangukia.” Viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliposikia simulizi hizi, wakajua kuwa Yesu alikuwa anawasema wao. Walitaka kumkamata Yesu. Lakini waliogopa kwani watu waliamini kuwa Yesu ni nabii. Yesu aliendelea kuwajibu viongozi wa Kiyahudi kwa mifano zaidi. Akasema, “Ufalme wa Mungu unafanana na jambo lililotokea mfalme alipoandaa sherehe ya harusi kwa ajili ya mwanaye. Aliwaalika baadhi ya watu. Wakati ulipofika mfalme aliwatuma watumwa wake kuwaambia watu waende kwenye sherehe. Lakini walikataa kwenda kwenye sherehe ya mfalme. Ndipo mfalme aliwaita baadhi ya watumishi wengine zaidi na akawaambia namna ya kuwaambia wale aliowaalika: ‘Njooni sasa! Sherehe imeandaliwa. Nimechinja ng'ombe wangu madume na ndama wanono waliolishwa nafaka, na kila kitu kiko tayari kuliwa. Njooni kwenye sherehe ya harusi.’ Lakini watu walioalikwa hawakujali yale waliyoambiwa na watumwa wa mfalme. Wengine waliondoka wakaenda kufanya mambo mengine. Mmoja alikwenda shambani na mwingine alikwenda kwenye shughuli zake. Wengine waliwakamata watumwa wa mfalme, wakawapiga na kuwaua. Mfalme alikasirika sana na akatuma jeshi lake kuwaua wale waliowaua watumwa wake. Na jeshi likauchoma moto mji wao. Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Sherehe ya harusi iko tayari. Niliwaalika wale watu lakini hawakustahili. Hivyo nendeni kwenye pembe za mitaa na mwalikeni kila mtu mtakayemwona, waambieni waje kwenye sherehe yangu.’ Hivyo watumwa wake waliingia mitaani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wabaya na wema na kuwaleta kwenye sherehe. Na jumba la sherehe likawa na wageni wengi. Mfalme alipoingia ili kuwasalimu wageni, alimwona mtu ambaye hakuwa amevaa vazi rasmi la harusi. Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki ilikuwaje ukaruhusiwa kuingia humo? Hujavaa vazi nadhifu kwa arusi!’ Lakini mtu yule hakuwa na neno la kusema. Hivyo mfalme akawaambia baadhi ya wale waliokuwa wanawahudumia watu kwa chakula, ‘Mfungeni mtu huyu mikono na miguu yake na mtupeni gizani, ambako watu wanalia na kusaga meno yao kwa maumivu.’ Ndiyo, watu wengi wamealikwa, lakini wachache tu ndiyo waliochaguliwa.” Kisha Mafarisayo wakaondoka mahali ambapo Yesu alikuwa anafundisha. Wakapanga mpango wa kumfanya aseme kitu ambacho wangekitumia dhidi yake. Wakawatuma kwake baadhi ya wafuasi wao na baadhi ya watu kutoka katika kundi la Maherode. Watu hawa walipofika kwa Yesu wakasema, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mtu mwema na kwamba daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu, bila kujali ni nani anakusikiliza. Huna wasiwasi namna ambavyo wengine wanaweza wakasema. Sasa tuambie, unadhani ni sahihi kulipa kodi kwa Kaisari au la?” Lakini Yesu alijua kuwa watu hawa walikuwa wanamtega. Hivyo akasema, “Enyi wanafiki! Kwa nini mnajaribu kunitega ili niseme jambo lililo kinyume? Nionesheni sarafu inayotumika kulipa kodi.” Wakamwonesha Yesu sarafu iliyotengenezwa kwa fedha. Kisha Yesu akauliza, “Picha iliyo kwenye sarafu hii ni ya nani? Na jina lililo kwenye sarafu hii ni la nani?” Wakajibu, “Ni picha ya Kaisari na ni jina la Kaisari.” Ndipo Yesu akawajibu, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake na mpeni Mungu vilivyo vyake.” Waliposikia yale Yesu aliyosema, wakashangaa na kuondoka. Siku hiyo hiyo baadhi ya Masadukayo walimjia Yesu. (Masadukayo hawaamini kuwepo kwa ufufuo wa wafu.) Masadukayo walimwuliza Yesu swali. Wakasema, “Mwalimu, Musa alituambia kuwa ikiwa mwanaume aliyeoa atakufa na hana watoto, ndugu yake lazima amwoe mkewe ili aweze kuzaa watoto kwa ajili ya nduguye aliyekufa. Walikuwepo ndugu saba miongoni mwetu. Ndugu wa kwanza alioa lakini akafa bila ya kupata watoto. Hivyo ndugu yake akamwoa mkewe. Na ndugu wa pili akafa pia, jambo hili hilo likatokea kwa ndugu wa tatu na ndugu wengine wote. Mwanamke akawa wa mwisho kufa. Lakini wanaume wote saba walikuwa wamemwoa. Sasa watu watakapofufuliwa kutoka kwa wafu, mwanamke huyu atakuwa mke wa yupi?” Yesu akajibu, “Mnakosea sana! Hamjui kile ambacho Maandiko yanasema. Na hamjui lolote kuhusu nguvu ya Mungu. Watu watakapofufuliwa kutoka kwa wafu, wanaume hawataoa wake na wanawake hawataozwa kwa wanaume. Kila mtu atakuwa kama malaika walio mbinguni. Someni kile ambacho Mungu alikisema kuhusu watu kufufuliwa kutoka kwa wafu. Mungu alisema, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’ Ni Mungu wa walio hai tu, hivyo hakika watu hawa hawakuwa wafu.” Watu waliposikia hili, waliyashangaa mafundisho ya Yesu. Mafarisayo waliposikia kuwa Yesu amewafanya Masadukayo waonekane wajinga nao wakaacha kumwuliza maswali. Kwa hiyo Mafarisayo wakafanya mkutano. Ndipo mmoja wao, aliye mtaalamu wa Sheria ya Musa, akamwuliza Yesu swali ili kumjaribu. Akasema, “Mwalimu, amri ipi katika sheria ni ya muhimu zaidi?” Yesu akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na akili yako yote.’ Hii ndiyo amri ya kwanza na ya muhimu zaidi. Na amri ya pili ni kama ya kwanza: ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’ Sheria yote na maandiko ya manabii yamejengwa katika amri hizi mbili.” Hivyo Mafarisayo walipokuwa pamoja, Yesu aliwauliza swali. Akasema, “Nini mawazo yenu juu ya Masihi? Je, ni mwana wa nani?” Mafarisayo wakajibu, “Masihi ni Mwana wa Daudi.” Yesu akawaambia, “Sasa ni kwa nini Daudi anamwita ‘Bwana’? Daudi alikuwa anazungumza kwa nguvu ya Roho. Aliposema, ‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu: Keti karibu nami upande wangu wa kuume, na nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’ Ikiwa Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Inakuwaje Masihi ni mwana wa Daudi?” Hakuna Farisayo aliyeweza kumjibu Yesu. Na baada ya siku hiyo, hakuna aliyekuwa jasiri kumwuliza maswali zaidi. Kisha Yesu akazungumza na watu pamoja na wafuasi wake, akasema, “Walimu wa sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kuwaambia Sheria ya Musa inasema nini. Hivyo mnapaswa kuwatii. Fanyeni kila wanachowaambia. Lakini maisha yao sio mfano mzuri wa kuufuata. Hawatendi wale wanayofundisha. Hutengeneza orodha ndefu ya kanuni na kujaribu kuwalazimisha watu kuzifuata. Lakini sheria hizi ni kama mizigo mizito ambayo watu hawawezi kuibeba, na viongozi hawa hawatazirahisisha kupunguza mzigo kwa watu. Wao wanatenda mambo mema tu ili waonwe na watu wengine. Hufanya visanduku vidogo vya Maandiko wanavyovaa kuwa vikubwa zaidi. Hufanya mashada ya urembo kwenye mavazi yao ya nje kuwa marefu zaidi ili waonwe na watu. Watu hawa wanapenda kukaa sehemu za heshima kwenye sherehe na kwenye viti muhimu zaidi katika masinagogi. Wanapenda kuitwa ‘Mwalimu’ Na kusalimiwa kwa heshima na watu kwenye masoko. Ninyi nyote ni ndugu, dada na kaka kwa sababu mnaye mwalimu mmoja tu. Hivyo msikubali kuitwa ‘Mwalimu’. Nanyi msimwite mtu yeyote duniani ‘Baba’, maana mnaye Baba mmoja tu, naye yuko mbinguni. Msikubali kuitwa ‘Mwalimu’, kwa sababu mnaye Mwalimu mmoja tu, naye ni Masihi. Kila atakayetumika kama mtumishi ndiyo mkuu zaidi kati yenu. Wanaojifanya kuwa bora kuliko wengine watanyenyekezwa kwa lazima. Lakini watu wanaojinyenyekeza wenyewe watafanywa kuwa wakuu. Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnawafungia watu njia ya kuingia katika ufalme wa Mungu, kwa kuwa ninyi wenyewe hamwingii na mnawazuia wale wanaojaribu kuingia. *** Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki. Mnasafiri kuvuka bahari na nchi nyingine ili kumtafuta mtu mmoja atakayefuata njia zenu. Mnapompata mtu huyo, mnamfanya astahili maradufu kwenda Jehanamu kama ninyi mlivyo! Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona. Mnasema, ‘Mtu yeyote akiweka kiapo au nadhiri kwa jina la Hekalu, haimaanishi kitu. Lakini yeyote atakayeweka kiapo kwa kutumia dhahabu iliyo Hekaluni lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ Ninyi ni wasiyeona mlio wajinga! Hamwoni kuwa Hekalu ni kuu kuliko dhahabu iliyo ndani yake? Hekalu ndilo huifanya dhahabu kuwa takatifu! Na mnasema, ‘Mtu yeyote akitumia madhabahu kuweka nadhiri au kiapo, haina maana yeyote. Lakini kila anayetumia sadaka iliyo kwenye madhabahu na kuapa au kuweka nadhiri, lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ Ninyi ni wasiyeona! Hamwoni kuwa madhabahu ni kuu kuliko sadaka yo yote iliyo juu yake? Madhabahu ndiyo inaifanya sadaka kuwa takatifu! Kila anayeitumia madhabahu kuapa au kuweka nadhiri ni dhahiri anatumia madhabahu na kila kitu kilicho juu yake. Na kila anayetumia Hekalu kuapa au kuweka nadhiri kwa hakika analitumia Hekalu na Mungu, anayeishi ndani humo. Kila anayetumia mbingu kuapa au kuweka nadhiri anakitumia kiti cha enzi cha Mungu na yule aketiye juu yake. Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya chakula mnachopata, hata mnanaa, binzari na jira. Lakini hamtii mambo ya muhimu katika mafundisho ya sheria; kuishi kwa haki, kuwa wenye huruma, na kuwa waaminifu. Haya ndiyo mambo mnayopaswa kufanya. Na mwendelee pia kufanya mambo hayo mengine. Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona! Ninyi ni kama mtu anayemtoa nzi katika kinywa chake na kisha anammeza ngamia! Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnaosha vikombe na sahani zenu kwa nje. Lakini ndani yake vimejaa vitu mlivyopata kwa kuwadang'anya wengine na kujifurahisha ninyi wenyewe. Mafarisayo, ninyi ni wasiyeona! Safisheni kwanza vikombe kwa ndani ili viwe safi. Ndipo vikombe hivyo vitakuwa safi hata kwa nje. Ole wenu walimu wa sheria na ninyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Ninyi ni kama makaburi yaliyopakwa rangi nyeupe, lakini ndani yake yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. Ndivyo ilivyo hata kwenu. Watu wanawatazama na kudhani kuwa ninyi ni wenye haki, lakini mmejaa unafiki na uovu ndani yenu. Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii, na kuyaheshimu makaburi ya wenye haki waliouawa. Na mnasema, ‘Ikiwa tungeishi nyakati za mababu zetu, tusingewasaidia kuwaua manabii hawa.’ Hivyo mnathibitisha kuwa ninyi ni uzao wa wale waliowaua manabii. Na mtaimalizia dhambi waliyoianza mababu zenu! Enyi nyoka! Ninyi mlio wa uzao wa nyoka wenye sumu kali! Hamtaikwepa adhabu. Mtahukumiwa na kutupwa Jehanamu! Hivyo ninawaambia: Ninawatuma manabii na walimu wenye hekima na wanaojua Maandiko. Lakini mtawaua, mtawatundika baadhi yao kwenye misalaba na kuwapiga wengine katika masinagogi yenu. Mtawafukuza kutoka katika mji mmoja hadi mwingine. Hivyo mtakuwa na hatia kutokana vifo vyote vya watu wema wote waliouawa duniani. Mtakuwa na hatia kwa kumwua mtu wa haki Habili, na mtakuwa na hatia kwa kuuawa kwa Zakaria mwana wa Barakia mliyemwua kati ya Hekalu na madhabahu. Mtakuwa na hatia ya kuwaua watu wote wema walioishi kati ya wakati wa Habili mpaka wakati wa Zakaria. Niaminini ninapowaambia kuwa mambo haya yote yatawapata ninyi watu mnaoishi sasa. Ee Yerusalemu, Yerusalemu! Unayewaua manabii. Unawapiga kwa mawe wale ambao Mungu amewatuma kwako. Mara nyingi nimetaka kuwasaidia watu wako. Nimetaka kuwakusanya watu wako kama kuku anavyowakusanya vifaranga wake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu kufanya hivyo. Sasa Hekalu lako litaachwa ukiwa kabisa. Ninakwambia, hautaniona tena mpaka wakati utakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’” Yesu alipokuwa anaondoka eneo la Hekalu, wanafunzi wake walimwendea na kumwonyesha majengo ya Hekalu. Akawauliza, “Mnayaona majengo haya? Ukweli ni kuwa, yataharibiwa. Kila jiwe litadondoshwa chini, hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jiwe jingine.” Baadaye, Yesu alipokuwa ameketi mahali fulani katika Mlima wa Mizeituni, Wafuasi wake walimwendea faraghani. Wakasema, “Twambie mambo haya yatatokea lini. Na nini kitatokea ili kutuandaa kwa ajili ya ujio wako na mwisho wa nyakati?” Yesu akajibu, “Mjihadhari! Msimruhusu mtu yeyote awadanganye. Watu wengi watakuja na watatumia jina langu. Watasema, ‘Mimi ndiye Masihi.’ Na watawadanganya watu wengi. Mtasikia kuhusu vita vinanavyopiganwa na pia matetesi ya kuwapo vita vingine. Lakini msiogope. Mambo haya lazima yatokee na mwisho wenyewe hautafuata palepale. Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. Utakuwepo wakati wa njaa ambapo watu watakosa chakula. Na kutakuwa matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. Mambo haya ni mwanzo wa matatizo, kama uchungu wa kwanza mwanamke anapozaa. Kisha mtakamatwa na kupelekwa kwa wenye mamlaka ili mhukumiwe na kuuawa. Watu wote katika ulimwengu watawachukia kwa sababu mnaniamini mimi. Nyakati hizo watu wengi wataacha kuwa wafuasi wangu. Watasalitiana na kuchukiana. Manabii wengi watatokea na kusababisha watu wengi kuamini mambo yasiyo ya kweli. Kutakuwepo na uovu mwingi sana duniani kiasi kwamba upendo wa waaminio wengi utapoa. Lakini yeyote yule atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. Na Habari Njema niliyoihubiri kuhusu Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote. Itatawanywa katika kila taifa. Kisha mwisho utakuja. Nabii Danieli alizungumza kuhusu ‘jambo la kutisha litakalosababisha uharibifu.’ Mtakapoliona jambo hili la kutisha limesimama patakatifu.” (Asomaye hili anapaswa kuelewa jambo hili linamaanisha nini.) “Watu walio Uyahudi wakimbilie milimani. Wakimbie pasipo kupoteza muda ili kuchukua kitu chochote. Wakiwa darini wasiteremke ili kuchukua kitu na kukitoa nje ya nyumba. Wakiwa shambani wasirudi nyumbani kuchukua koti. Itakuwa hali ngumu kwa wanawake wenye mimba na wenye watoto wachanga! Ombeni isiwe majira ya baridi au isiwe siku ya Sabato mambo haya yatakapotokea na mkalazimika kukimbia, kwa sababu utakuwa wakati wa dhiki kuu. Kutakuwepo na usumbufu mwingi sana kuliko ule uliowahi kutokea tangu mwanzo wa ulimwengu. Na hakuna jambo baya kama hilo litakalotokea tena. Lakini Mungu amekwisha amua kuufupisha wakati huo. Ikiwa usingefupishwa, hakuna ambaye angeendelea kuishi. Lakini Mungu ataufupisha ili kuwasaidia watu aliowachagua. Wakati huo watu wataweza kuwaambia, ‘Tazama, Masihi yuko kule!’ Au wakasema, ‘Ni yule!’ Msiwaamini. Manabii wa uongo na masihi wa uongo watatokea na kufanya miujiza na maajabu makuu, ili ikiwezekana wawadanganye wateule. Na sasa nimewatahadharisha kuhusu hili kabla halijatokea. Inawezekana mtaambiwa, ‘Masihi yuko jangwani!’ Msiende jangwani kumtafuta. Mtu mwingine anaweza akasema, ‘Masihi yuko katika chumba kile!’ Msiamini. Mwana wa Adamu atakapokuja, kila mtu atamwona. Itakuwa kama radi inavyowaka angani na kuonekana kila mahali. Ni kama kutafuta mzoga: Mzoga hupatikana mahali ambapo tai wengi wamekusanyika. Mara baada ya mateso ya siku hizo, mambo haya yatatokea: ‘Jua litakuwa jeusi, na mwezi hautatoa mwanga. Nyota zitaanguka kutoka angani, na kila kitu kilicho angani kitatikiswa kutoka mahali pake.’ Kisha kutatokea ishara angani kuwa Mwana wa Adamu anakuja. Watu wote wa ulimwengu watajipiga kifuani wakiomboleza. Kila mtu atamwona Mwana wa Adamu akija katika mawingu ya angani akiwa na nguvu na utukufu mkuu. Naye atatumia parapanda kuu kuwatuma malaika zake kila mahali duniani. Nao watawakusanya wateule wake kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine. Jifunze kwa mtini: Matawi yake yanapokuwa ya kijani na laini na kuanza kutoa majani mapya, ndipo mnatambua kuwa majira ya joto yamekaribia. Katika namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yakitokea, mtajua kuwa wakati umekaribia wa kile kitakachotokea. Ninawahakikishia kuwa mambo haya yote yatatokea wakati ambao baadhi ya watu wa nyakati hizi wakiwa bado hai. Ulimwengu wote, dunia na anga vitaangamizwa, lakini maneno yangu yatadumu milele. Hakuna anayeijua siku wala wakati. Malaika wa mbinguni hawaijui hata Mwana hajui itakuwa lini. Baba peke yake ndiye anayejua. Mwana wa Adamu atakapokuja, itakuwa kama ilivyokuwa nyakati za Nuhu. Siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuwatoa binti zao kuolewa mpaka siku ambayo Nuhu aliingia kwenye safina. Hawakujua juu ya kilichokuwa kinaendelea mpaka mafuriko yalipowajia na kuwaangamiza wote. Ndiyo itakavyokuwa Mwana wa Adamu atakapokuja. Wanaume wawili watakuwa wakifanya kazi shambani, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. Hivyo iweni tayari daima. Hamjui siku ambayo Bwana wenu atarudi. Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua wakati ambao mwizi atakuja? Mnajua angelikesha ili mwizi asivunje na kuingia. Hivyo, ninyi nanyi iweni tayari. Mwana wa Adamu atakuja katika wakati msiomtarajia. Fikiria mtumishi aliyewekwa na bwana wake kuwapa chakula watumishi wake wengine katika muda uliopangwa. Ni kwa namna gani mtumishi huyo atajionyesha kuwa ni mwangalifu na mwaminifu? Bwana wake atakaporudi na kumkuta anafanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha kwa mtumishi huyo. Ninawaambia bila mashaka yoyote kuwa, bwana wake atamchagua mtumishi huyo awe msimamizi wa kila kitu anachomiliki yule Bwana. Lakini nini kitatokea ikiwa mtumishi huyo ni mbaya na akadhani kuwa bwana wake hatarudi karibuni? Ataanza kuwapiga watumishi wengine na kuanza kunywa na kula na walevi. Ndipo bwana wake atakuja wakati asioutarajia, ambapo mtumishi hakujiandaa. Bwana atamwadhibu mtumishi huyo na kumpeleka anakostahili kuwapo pamoja na watumishi wengine waliojifanya kuwa wema. Huko watalia na kusaga meno kwa maumivu. Nyakati hizo, ufalme wa Mungu utafanana na wanawali kumi waliokwenda kusubiri kuwasili kwa bwana arusi wakiwa na taa zao. Watano kati yao walikuwa na hekima, na watano walikuwa wajinga. Wanawali wajinga walichukua taa zao bila ya kubeba mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao. Wanawali wenye hekima walichukua taa zao pamoja na mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao katika chupa. Bwana arusi alipochelewa sana, walichoka na wote wakasinzia. Usiku wa manane ulipofika, ikatangazwa, ‘Bwana arusi anakuja! Njooni mumlaki!’ Wasichana wote waliamka. Wakatayarisha taa zao. Lakini wanawali wajinga wakawaambia wanawali wenye hekima, ‘Tupeni mafuta kiasi kwa sababu mafuta katika taa zetu yamekwisha.’ Wanawali wenye hekima wakajibu, ‘Hapana! Mafuta tuliyonayo hayatatutosha sisi sote. Lakini nendeni kwa wauza mafuta mkanunue.’ Hivyo wanawali wajinga wakaenda kununua mafuta. Walipoondoka, bwana arusi akafika. Wanawali waliokuwa tayari wakaingia kwenye sherehe ya arusi pamoja na bwana arusi. Kisha mlango ukafungwa. Baadaye wanawali waliokwenda kununua mafuta wakarudi. Wakasema, ‘bwana, bwana! Fungua mlango tuingie.’ Lakini bwana arusi akajibu, ‘Kwa hakika hapana! Wala siwajui ninyi.’ Hivyo iweni tayari kila wakati. Hamjui siku wala muda ambao Mwana wa Adamu atakuja. Pia, ufalme wa Mungu unafanana na mtu aliyekuwa akiondoka nyumbani kwake kusafiri safari ndefu. Aliwaita watumishi wake na kuwaweka kuwa wasimamizi wa mali zake. Alimgawia kila mtumishi kiasi cha mali atakachosimamia. Alimpa mmoja talanta tano. Alimpa mtumishi mwingine talanta mbili na akampa mtumishi wa tatu talanta moja. Kisha akaondoka. Mtumishi aliyepewa talanta tano alikwenda akazifanyia biashara na talanta zile tano zikazaa talanta tano zingine. Mtumishi aliyepewa talanta mbili alifanya vivyo hivyo. Mtumishi huyo alizifanyia biashara talanta mbili alizopewa na zikazaa talanta mbili zingine. Lakini mtumishi aliyekabidhiwa talanta moja, alikwenda akachimba shimo kisha akaifukia talanta moja aliyopewa na bwana wake. Baada ya muda mrefu kupita bwana wao alirudi. Aliwauliza watumishi wake walizifanyia nini talanta alizowaachia. Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano alimletea bwana wake talanta tano alizomwachia na talanta zingine tano zaidi. Mtumishi akamwambia bwana wake, ‘Bwana, uliniamini ukaniachia talanta tano kuzitunza, hivyo nilizifanyia biashara na kupata talanta tano zaidi.’ Bwana wake akajibu, ‘Ulifanya vyema. Wewe ni mtumishi mwema unayeweza kuaminiwa. Ulifanya vizuri kwa kiasi kidogo hicho cha pesa. Hivyo nitakufanya kuwa msimamizi wa mambo makuu. Njoo usherehekee pamoja nami.’ Kisha mtumishi aliyepewa talanta mbili akaja kwa bwana wake. Akasema, ‘Bwana ulinipa talanta mbili ili nizitunze. Nilizifanyia biashara talanta hizi mbili na nimepata zingine mbili zaidi.’ Bwana wake akajibu, ‘Ulifanya vyema. Wewe ni mtumishi mwema unayeweza kuaminiwa. Ulifanya vizuri kwa kiasi kidogo hicho cha pesa. Hivyo nitakufanya kuwa msimamizi wa mambo makuu. Njoo usherehekee pamoja nami.’ Ndipo mtumishi aliyeachiwa talanta moja akaja kwa bwana wake. Akasema, ‘Bwana, nilijua wewe ni mkorofi sana. Unavuna usichopanda. Unakusanya mazao mahali ambapo hukupanda mbegu yoyote. Hivyo niliogopa. Nilienda nikaificha talanta yako ardhini. Hii hapa ni ile talanta moja ya fedha uliyonipa.’ Bwana wao akamjibu, ‘Wewe ni mtumishi mbaya na mvivu! Unasema kwamba ulijua ninavuna nisichopanda na ninakusanya mazao ambayo sikupanda mbegu yo yote. Hivyo ungeweka pesa yangu benki. Kisha, wakati nitakaporudi ningepata talanta yangu pamoja na faida ambayo ingezalishwa na talanta yangu.’ Hivyo bwana wao akawaambia watumishi wake wengine, ‘Mnyang'anyeni talanta moja mtumishi huyo na kumpa mtumishi mwenye talanta kumi. Kila aliyezalisha faida atapata zaidi. Atakuwa na vingi kuzidi mahitaji yake. Lakini wale wasiotumia walivyonavyo kuleta faida watanyang'anywa kila kitu.’ Kisha bwana wao akasema, ‘Mtupeni nje, gizani mtumishi huyo asiyefaa, ambako watu watalia na kusaga meno kwa maumivu.’ Mwana wa Adamu atakuja akiwa katika utukufu wake, pamoja na malaika wote. Ataketi kwenye kiti chake cha enzi akiwa mfalme. Watu wote wa ulimwenguni watakusanywa mbele zake, kisha atawagawa katika makundi mawili. Itakuwa kama mchungaji anavyowatenga kondoo kutoka katika kundi la mbuzi. Atawaweka kondoo upande wake wa kuume na mbuzi upande wa kushoto. Kisha mfalme atawaambia walio upande wake wa kuume, ‘Njooni, baba yangu ana baraka kuu kwa ajili yenu. Ufalme alioahidi ni wenu sasa. Uliandaliwa kwa ajili yenu tangu dunia ilipoumbwa. Ni wenu kwa sababu nilipokuwa na njaa, mlinipa chakula. Nilipokuwa na kiu, mlinipa maji ya kunywa. Nilipokosa mahali pa kukaa, mlinikaribisha katika nyumba zenu. Nilipokosa nguo, mlinipa mavazi ya kuvaa. Nilipokuwa mgonjwa, mlinijali. Nilipofungwa gerezani, mlikuja kunitembelea.’ Kisha wenye haki watajibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakupa chakula? Lini tulikuona una kiu tukakupa maji ya kunywa? Lini tulikuona huna mahali pa kukaa tukakukaribisha katika nyumba zetu? Lini tulikuona huna nguo za kuvaa na tukakuvisha? Lini tulikuona unaumwa au uko gerezani tukaja kukuona?’ Kisha mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, kila mlichowafanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si watu wa thamani, mlinifanyia mimi pia.’ Kisha mfalme atawaambia walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu. Mungu amekwisha amua kuwa mtaadhibiwa. Nendeni katika moto uwakao milele, moto ulioandaliwa kwa ajili ya yule Mwovu na malaika zake. Ondokeni kwa sababu nilipokuwa na njaa, hamkunipa chakula nile. Nilipokuwa na kiu, hamkunipa maji ya kunywa. Nilipokosa mahali pa kukaa, hamkunikaribisha katika nyumba zenu. Nilipokosa nguo za kuvaa, hamkunipa nguo za kuvaa. Nilipokuwa mgonjwa au mfungwa gerezani hamkunijali.’ Ndipo watu hao watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu? Lini tulikuona huna mahali pa kukaa? Au ni lini tulikuona huna nguo au mgonjwa au ukiwa gerezani? Tuliona haya yote lini na hatukukusaidia?’ Mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, chochote mlichokataa kumfanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si wa muhimu, mlikataa kunifanyia mimi.’ Ndipo watu hawa watakapondolewa ili kuadhibiwa milele. Lakini wenye haki watakwenda kuyafurahia maisha ya milele.” Yesu alipomaliza akasema haya yote, akawaambia wafuasi wake, “Mnajua kuwa kesho kutwa ni Pasaka. Siku hiyo Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwa maadui zake ili auawe msalabani.” Ndipo viongozi wa makuhani na wazee walikutana katika nyumba ya Kayafa kuhani mkuu. Katika mkutano huo walitafuta njia ya kumkamata na kumwua Yesu kwa siri pasipo mtu yeyote kujua. Wakasema, “Hatuwezi kumkamata Yesu wakati wa sherehe ya Pasaka. Hatutaki watu wakasirike na kusababisha vurugu.” Yesu alipokuwa Bethania katika nyumba ya Simoni aliyekuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Mwanamke alimwendea, akiwa na chupa yenye manukato ya thamani kubwa. Yesu akiwa anakula, mwanamke huyo akamwagia manukato hayo kichwani. Wanafunzi walipomwona mwanamke akifanya hivi walimkasirikia. Walisema, “Kwa nini kuharibu manukato hayo? Yangeuzwa na pesa nyingi ingepatikana, na pesa hiyo wangepewa maskini.” Lakini Yesu alijua kilichokuwa kinaendelea. Akasema, “Kwa nini mnamsumbua mwanamke huyu? Amenifanyia jambo zuri sana. Mtaendelea kuishi na maskini siku zote. Lakini ninyi hamtakuwa nami siku zote. Mwanamke huyu amenimwagia manukato. Amefanya hivi kuniandaa kwa ajili ya mazishi baada ya kufa. Habari Njema itahubiriwa kwa watu wote ulimwenguni. Na ninaweza kuwathibitishia kuwa kila mahali ambako Habari Njema zitahubiriwa, jambo alilofanya mwanamke huyu litahubiriwa pia, na watu watamkumbuka.” Ndipo Yuda Iskariote, mmoja wa wanafunzi kumi na wawili wa Yesu alikwenda kuzungumza na wakuu wa makuhani. Akasema, “Nikimkabidhi Yesu kwenu, mtanilipa nini?” Makuhani walimpa sarafu thelathini za fedha. Kuanzia siku hiyo, Yuda alianza kutafuta muda mzuri wa kumsaliti Yesu. Ilipofika siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wafuasi wake walimjia Yesu na kumwambia, “Tutaandaa kila kitu kwa ajili yako ili ule mlo wa Pasaka. Unataka tuandae wapi mlo wa Pasaka?” Yesu akajibu, “Nendeni mjini kwa mtu ninayemfahamu. Mwambieni kuwa Mwalimu anasema, ‘Muda uliowekwa kwa ajili yangu umekaribia sana. Mimi na wafuasi wangu tutakula mlo wa Pasaka katika nyumba yako.’” Walitii na kufanya kama Yesu alivyowaambia. Waliandaa mlo wa Pasaka. Jioni ilipowadia, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakila Yesu akasema, “Niaminini, ninapowaambia kuwa mmoja wenu ninyi kumi na wawili atanikabidhi kwa maadui zangu.” Wanafunzi walisikitika sana waliposikia hili. Kila mmoja akasema, “Bwana, hakika si mimi!” Yesu akajibu, “Yeye aliyechovya mkate wake katika kikombe kile kile nilichochovya mimi ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu atakiendea kifo chake kama Maandiko yanavyosema. Lakini ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Adamu ili auawe. Ni bora mtu huyo asingezaliwa.” Ndipo Yuda, ambaye ndiye angemsaliti, akamwambia Yesu, “Mwalimu, hakika si mimi unayemzungumzia, ama ndiye?” Yesu akamjibu, “hicho ndicho unachosema.” Walipokuwa wakila, Yesu alichukua baadhi ya mikate na akamshukuru Mungu. Alimega baadhi ya vipande, akawapa wafuasi wake na akasema, “Chukueni mkate huu na mle. Ni mwili wangu.” Kisha akachukua kikombe chenye divai, akamshukuru Mungu na akawapa. Akasema, “Kila mmoja wenu anywe divai iliyo katika kikombe hiki. Divai hii ni damu yangu, itakayomwagika ili kusamehe dhambi za watu wengi na kuanza Agano Jipya ambalo Mungu analifanya na watu wake. Ninataka mjue kuwa, hii ni mara ya mwisho nitakunywa divai mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.” Waliimba wimbo kwa pamoja kisha wakaenda kwenye Mlima wa Mizeituni. Yesu akawaambia wafuasi wake, “Usiku wa leo ninyi nyote mtapoteza imani yangu kwangu. Maandiko yanasema, ‘Nitamwua mchungaji, na kondoo watatawanyika.’ Lakini baada ya kuuawa, nitafufuka Kisha nitakwenda Galilaya. Nitakuwa huko kabla ninyi hamjaenda huko.” Petro akajibu, “Wafuasi wengine wote wanaweza kupoteza imani juu yako. Lakini imani yangu haitatetereka.” Yesu akajibu, “Ukweli ni huu, usiku wa leo utasema haunifahamu. Utanikana mara tatu kabla jogoo hajawika.” Lakini Petro akajibu, “Sitasema kwamba sikufahamu! Mimi hata nitakufa pamoja nawe!” Na wafuasi wengine wote wakasema kitu hicho hicho. Kisha Yesu akaondoka pamoja na wafuasi wake na kwenda mahali panapoitwa Gethsemane. Akawaambia, “Kaeni hapa wakati ninakwenda mahali pale kuomba.” Alimwambia Petro na wana wawili wa Zebedayo waende pamoja naye. Kisha akaanza kuhuzunika na kuhangaika. Yesu akamwambia Petro na wana wa Zebedayo, “Moyo wangu ni mzito na wenye huzuni hata kujisikia kana kwamba huzuni hiyo itaniua. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.” Kisha Yesu akaenda mbele kidogo. Akainama hadi chini uso wake ukiigusa nchi akiomba na akasema, “Baba yangu, ikiwezekana, usifanye nikinywee kikombe hiki cha mateso. Lakini fanya lile ulitakalo na si lile ninalolitaka mimi.” Kisha akarudi walipokuwa wafuasi wake na akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Je hamkuwa na uwezo wa kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? Amkeni kesheni na kuomba ili muyashinde majaribu. Roho zenu zinataka kufanya mambo sahihi, lakini miili yenu ni dhaifu.” Kisha Yesu akaenda mara ya pili na akaomba akisema, “Baba yangu, ikiwa ni lazima nikinywee kikombe hiki na haiwezekani nikakwepa, basi mapenzi yako na yatimizwe.” Kisha akarudi na kwenda walipokuwa wafuasi wake, akawakuta wamelala tena. Hawakuweza kukesha. Hivyo akawaacha akaenda tena kuomba. Mara hii ya tatu alipokuwa anaomba akasema kama alivyosema hapo mwanzo. Kisha Yesu akawarudia wafuasi wake na akasema, “Bado mnalala na kupumzika? Wakati wa Mwana wa Adamu kukabidhiwa kwa wenye dhambi umewadia. Simameni! Tuondoke. Tazama yeye atakayenikabidhi anakuja.” Yesu alipokuwa anazungumza, Yuda mmoja wa wanafunzi wake kumi na mbili alifika akiwa na kundi kubwa la watu, waliokuwa wamebeba majambia na marungu. Walikuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. Yuda aliyekuwa amkabidhi Yesu kwao, alipanga kufanya kitu cha kuwajulisha yupi kati ya wafuasi alikuwa Yesu. Alisema, “Mtu nitakayembusu ndiye mtakayemkamata.” Hivyo Yuda alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Salamu, Mwalimu!” Kisha akambusu. Yesu akajibu, “Rafiki yangu, fanya ulilokuja kufanya.” Kisha wale watu wakaja na kumkamata Yesu. Jambo hili lilipotokea, mmoja wa wafuasi wa Yesu alichukua jambia lake na kumkata sikio mtumishi wa kuhani mkuu. Yesu akamwambia, “Rudisha jambia lako mahali pake. Atumiaye jambia atauawa kwa jambia. Hakika unajua kuwa ningemwomba Baba yangu yeye angenipa zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika. Lakini hilo lisingekubaliana na yale Maandiko, yanayosema hivi ndivyo ilivyopasa itokee.” Kisha Yesu akaliambia kundi, “Kwa nini mnakuja kunikamata mkiwa na mikuki na marungu kama vile mimi ni mhalifu? Nimekuwa nakaa eneo la Hekalu nikifundisha kila siku. Kwa nini hamkunikamata kule? Lakini mambo haya yote yametokea ili kutimiza Maandiko yaliyoandikwa na manabii.” Ndipo wafuasi wake wote wakamwacha na kukimbia. Wale waliomkamata Yesu wakampeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu. Walimu wa Sheria na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwa wamekusanyika huko. Petro alimfuata Yesu lakini alikuwa mbali kidogo. Alimfuata mpaka katika ua wa nyumba ya kuhani mkuu. Petro alienda uani na akakaa pamoja na walinzi. Alitaka kuona nini kingetokea. Viongozi wa makuhani na baraza kuu walijaribu kutafuta kosa ili waweze kumwua Yesu. Walijaribu kutafuta watu ili wadanganye kuwa Yesu alifanya kosa. Watu wengi walikuja na akasema uongo kuhusu Yesu. Lakini baraza lilishindwa kupata ushahidi wa kuutumia ili kumwua. Ndipo watu wawili walikuja na akasema, “Mtu huyu alisema, ‘Ninaweza kuliharibu Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’” Kisha kuhani mkuu alisimama na kumwambia Yesu, “Huna neno lolote la kujitetea dhidi ya mashtaka haya juu yako? Wanasema kweli?” Lakini Yesu hakusema neno lolote. Kisha kuhani mkuu akamwambia Yesu, “Apa mbele za Mungu aliye hai kwamba utatuambia kweli. Je, wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu?” Yesu akajibu, “Unaweza akasema hivyo, Mimi ndiye. Lakini ninawaambia, kitambo kidogo mtamwona Mwana wa Adamu akiwa amekaa upande wa kuume wa Mungu, mwenye Nguvu. Na mtamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni.” Kuhani mkuu aliposikia hili, alilarua vazi lake kwa hasira. Akasema, “Mtu huyu amemtukana Mungu! Hatuhitaji mashahidi zaidi. Ninyi nyote mmesikia matusi yake. Mnasemaje?” Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ana hatia, na ni lazima afe.” Na baadhi ya waliokuwa pale wakamtemea mate Yesu usoni na kumpiga makonde na wengine walimpiga makofi. Wakasema, “Tuonyeshe kuwa wewe ni nabii, Masihi! Nani amekupiga!” Petro alipokuwa amekaa nje uani, msichana mtumishi akamwendea. Akasema, “Ulikuwa pamoja na Yesu, yule mtu kutoka Galilaya.” Lakini Petro akamwambia kila mtu aliyekuwa pale kuwa si kweli. Akasema “Sijui unachosema.” Kisha akaondoka uani. Akiwa kwenye lango msichana mtumishi akamwona na akawaambia watu waliokuwa pale, “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.” Kwa mara nyingine tena Petro akasema hakuwa pamoja na Yesu. Akasema, “Ninaapa kwa Mungu, simfahamu mtu huyu!” Baada ya muda mfupi baadaye, watu waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro na kumwambia, “Tunajua wewe ni mmoja wao. Hata namna unavyoongea inaonesha wazi kuwa ndivyo hivyo.” Kisha Petro akaanza kujiapiza mwenyewe ikiwa anaongopa. Akasema, “Ninaapa kwa Mungu, simfahamu mtu huyu!” Mara alipomaliza akasema hili, jogoo akawika. Kisha akakumbuka maneno alivyoambiwa na Yesu kuwa: “Kabla jogoo hajawika, utakuwa umenikana mara tatu.” Kisha Petro akatoka nje na kulia kwa uchungu sana. Mapema asubuhi, viongozi wote wa makuhani na viongozi wazee walikutana na kuamua kumwua Yesu. Wakamfunga kamba, wakamwondoa na kwenda kumkabidhi kwa Pilato, gavana wa Kirumi. Baada ya kumkabidhi Yesu, Yuda aliona kila kitu kilichotokea na kujua kuwa wameamua kumwua Yesu. Naye alihuzunika sana kutokana na kile alichokifanya. Hivyo alirudisha vile vipande thelathini vya sarafu vya fedha kwa wakuu wa makuhani na viongozi wazee. Yuda aliwaambia, “Nimetenda dhambi. Nimemsaliti kwenu mtu asiye na hatia ili auawe.” Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Hilo halituhusu. Ni tatizo lako, siyo letu sisi.” Hivyo Yuda akavitupa vipande thelathini vya fedha Hekaluni, kisha akatoka akaenda kujinyonga. Viongozi wa makuhani wakaviokota vile vipande vya fedha Hekaluni. Wakasema, “Sheria yetu haituruhusu kuweka fedha hii katika hazina ya Hekalu, kwa sababu fedha hii imelipwa kwa ajili ya kifo, ni fedha yenye damu.” Hivyo wakaamua kutumia fedha hiyo kwa kununulia shamba linaloitwa Shamba la Mfinyanzi kwa ajili ya kuwazikia wageni wanapokufa wakiwa ziarani katika mji wa Yerusalemu. Ndiyo sababu eneo hilo bado linaitwa Shamba la Damu. Hili lilitimiza maneno ya nabii Yeremia aliposema: “Walichukua sarafu thelathini za fedha. Hicho ni kiasi ambacho Waisraeli waliamua kulipa kwa ajili ya uhai wake. Walizitumia sarafu hizo thelathini za fedha kununulia shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniamuru.” Yesu alisimama mbele ya Gavana, Pilato, ambaye alimwuliza Yesu, “Wewe ni mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Waweza kusema hivyo.” Lakini viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi walipomshutumu, hakusema kitu. Hivyo Pilato akamwambia, “Husikii mashtaka haya yote wanayokushtaki wewe? Kwa nini hujibu?” Lakini Yesu hakujibu kitu, gavana alishangaa sana. Kila mwaka wakati wa Pasaka, gavana angemwachia huru mfungwa mmoja yeyote ambaye watu wangetaka aachiwe huru. Wakati huo alikuwepo mtu gerezani aliyejulikana kuwa ni mtu mbaya. Mtu huyu aliitwa Baraba. Kundi la watu lilipokusanyika, Pilato aliwaambia, “Nitamwacha huru mtu mmoja. Mnataka nani nimwache huru: Baraba au Yesu aitwaye Masihi?” Pilato alijua kuwa viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu walikuwa wanamwonea wivu. Pilato alipokuwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akamtumia ujumbe uliosema, “Usifanye jambo lolote juu ya huyo mtu. Hana hatia. Nimeota ndoto juu yake usiku, na ndoto hiyo imenihangaisha sana.” Lakini viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi waliwaambia watu waombe Baraba aachiwe huru na Yesu auawe. Pilato akasema, “Nina Baraba na Yesu. Je, mnataka nimwache huru yupi?” Watu wakajibu, “Baraba!” Pilato akauliza, “Sasa nimfanye nini Yesu, aitwaye Masihi?” Watu wote wakasema, “Mwue msalabani!” Pilato akauliza, “Kwa nini mnataka nimwue Yesu? Amefanya kosa gani?” Lakini walipaza sauti wakisema, “Mwue msalabani!” Pilato akaona hakuna jambo ambalo angefanya ili kubadili nia yao. Kiukweli ilionekana wazi kuwa kungetokea fujo. Hivyo alichukua maji na kunawa mikono yake mbele yao wote. Akasema, “Sina hatia na kifo cha mtu huyu. Ninyi ndio mnaofanya hili!” Watu wakajibu, “Tutawajibika kwa kifo chake sisi wenyewe na hata watoto wetu!” Kisha Pilato akamwachia huru Baraba. Na akawaambia baadhi ya askari wamchape Yesu viboko. Kisha akamkabidhi Yesu kwa askari ili akauawe msalabani. Kisha askari wa Pilato wakamchukua Yesu mpaka kwenye nyumba ya gavana, kikosi kizima cha wale askari kikakusanyika pamoja kumzunguka Yesu. Wakamvua nguo zake na kumvalisha kivazi chekundu. Kisha wakatengeneza taji kutokana na matawi ya miiba na kuiweka kwenye kichwa chake na wakaweka fimbo kwenye mkono wake wa kulia. Kisha kwa kumdhihaki, wakainama mbele zake. Wakasema, “Tunakusalimu, mfalme wa Wayahudi!” Walimtemea mate. Kisha wakachukua fimbo yake na kuanza kumpiga nayo kichwani. Baada ya kumaliza kumdhihaki, askari walimvua kivazi chekundu na kumvalisha nguo zake. Kisha wakamwongoza kwenda kuuawa msalabani. Askari walipokuwa wanatoka mjini wakiwa na Yesu, walimwona mtu mmoja kutoka Kirene aliyeitwa Simoni, na wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. Walifika mahali palipoitwa Golgotha. (Yaani “Eneo la Fuvu la Kichwa”.) Askari walimpa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo. Lakini alipoionja, alikataa kuinywa. Askari walimgongomea Yesu msalabani, kisha wakacheza kamari ili wagawane nguo za Yesu. Askari walikaa pale ili kumlinda. Wakaweka alama juu ya kichwa chake kuonesha mashtaka dhidi yake yaliyosema: HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. Wahalifu wawili waligongomewa kwenye misalaba pamoja na Yesu, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto wa Yesu. Watu waliokuwa wakipita pale walitikisa vichwa vyao na kumtukana Yesu matusi kwa kusema, “Ulisema ungeweza kubomoa Hekalu na kulijenga tena katika siku tatu. Jiokoe mwenyewe! Teremka chini kutoka kwenye huo msalaba ikiwa kweli wewe ni Mwana wa Mungu!” Viongozi wa Makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwepo pale pia. Nao pia walimdhihaki Yesu kama watu wengine walivyofanya. Walisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa yeye mwenyewe! Watu husema kuwa yeye ni mfalme wa Israeli. Ikiwa yeye ni mfalme, ashuke kutoka msalabani. Ndipo tutamwamini. Alimtumaini Mungu. Hivyo Mungu amwokoe sasa, ikiwa hakika Mungu anamtaka. Yeye mwenyewe alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’” Hata wale wahalifu wawili waliokuwa misalabani upande wa kulia na wa kushoto wa Yesu walimtukana. Ilipofika adhuhuri, giza liliifunika Israeli yote kwa muda wa masaa matatu. Yapata saa tisa alasiri Yesu alilia kwa sauti kuu akisema, “ Eloi, Eloi, lema sabakthani? ” yaani “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha peke yangu?” Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hili wakasema, “Anamwita Eliya.” Mtu mmoja alikimbia haraka akaenda kuchukua sponji, akaijaza siki, akaifunga kwenye fimbo na akanyoosha fimbo ili kumpa Yesu sponji ili anywe siki. Lakini wengine walisema, “Usimjali. Tunataka tuone ikiwa Eliya atakuja kumsaidia.” Yesu akalia kwa sauti kuu tena, kisha akafa. Yesu alipokufa, pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili. Mpasuko wake ulianzia juu mpaka chini. Kulitokea pia tetemeko la ardhi na miamba ilipasuka. Makaburi yalifunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa walifufuka kutoka kwa wafu. Walitoka makaburini. Na baada ya Yesu kufufuliwa kutoka kwa wafu, walikwenda kwenye mji mtakatifu wa Yerusalemu, na watu wengi waliwaona. Afisa wa jeshi na askari waliokuwa wanamlinda Yesu walitetemeka sana kwa kuogopa tetemeko la ardhi na kila walichokiona kikitokea. Wakasema, “Hakika alikuwa Mwana wa Mungu!” Wanawake wengi waliomfuata Yesu kutoka Galilaya kumhudumia walikuwepo pale wakiangalia wakiwa wamesimama mbali na msalaba. Miongoni mwao alikuwepo Mariamu Magdalena, Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu na pia mama yao Yakobo na Yohana alikuwepo pale. Jioni ile, mtu mmoja tajiri aliyeitwa Yusufu alikuja Yerusalemu. Alikuwa mfuasi wa Yesu kutoka katika mji wa Arimathaya. Alikwenda kwa Pilato na akamwomba mwili wa Yesu. Pilato akawaamuru askari wampe Yusufu wa Arimathaya mwili wa Yesu. Aliuchukua mwili na kuuvingirisha katika kitambaa mororo cha kitani safi. Yusufu akauzika mwili wa Yesu katika kaburi mpya alilokuwa amelichonga kwenye mwamba mlimani. Kisha akalifunga kaburi kwa kuvingirisha jiwe kubwa kuziba mlango wa kaburi. Baada ya kufanya hivi, akaondoka. Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu walikuwa wamekaa karibu na kaburi. Siku ile ilikuwa Siku ya Maandalizi. Siku iliyofuata, viongozi wa makuhani na Mafarisayo walimwendea Pilato. Wakamwambia, “Mkuu, tunakumbuka kuwa yule mwongo alipokuwa hai alisema, ‘Nitafufuka kutoka kwa watu katika siku tatu.’ Hivyo amuru ili kaburi lilindwe kwa siku tatu. Wafuasi wake wanaweza kuja na kujaribu kuiba mwili. Kisha wataweza kumwambia kila mtu kuwa alifufuka kutoka kwa wafu. Uongo huo utakuwa hatari zaidi ya hata waliyosema juu yake alipokuwa hai.” Pilato akasema, “Chukueni baadhi ya askari, na mwende mkalinde kaburi kwa namna mnavyojua.” Kisha walikwenda kaburini na kuliweka salama dhidi ya wezi. Walifanya hivi kwa kuliziba kwa jiwe langoni na kuwaweka askari wa kulinda kaburi. Alfajiri mapema siku iliyofuata baada ya siku ya Sabato, yaani siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu alikwenda kuliangalia kaburi. Ghafla malaika wa Bwana akaja kutoka mbinguni, na tetemeko kubwa likatokea. Malaika alikwenda kaburini na kulivingirisha jiwe kutoka kwenye mlango wa kaburi. Kisha akaketi juu ya jiwe. Malaika alikuwa anang'aa kama miali ya radi. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. Askari waliokuwa wanalinda kaburi walimwogopa sana malaika, walitetemeka kwa woga na wakawa kama watu waliokufa. Malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope. Ninajua mnamtafuta Yesu, aliyeuawa msalabani. Lakini hayupo hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu, kama alivyosema. Njooni mwone mahali ulipokuwa mwili wake. Nendeni haraka mkawaambie wafuasi wake, ‘Yesu amefufuka kutoka kwa wafu. Amekwenda Galilaya na atafika huko kabla yenu. Na mtamwona huko.’” Kisha malaika akasema, “Sasa nimewaambia.” Hivyo wanawake wakaondoka haraka kaburini. Waliogopa sana, lakini walijawa na furaha. Walipokuwa wanakimbia kwenda kuwaambia wafuasi wake kilichotokea, ghafla Yesu alisimama mbele yao. Akasema, “Salamu!” Wanawake wakamwendea wakamshika miguu na wakamwabudu. Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie wafuasi wangu waende Galilaya, wataniona huko.” Wanawake wakaenda kuwaambia wafuasi. Na wakati huo huo baadhi ya askari waliokuwa wanalinda kaburi waliingia mjini. Walikwenda kuwaambia viongozi wa makuhani kila kitu kilichotokea. Ndipo makuhani wakakutana na viongozi wazee wa Kiyahudi na kufanya mpango. Wakawalipa wale askari pesa nyingi na kuwaambia, “Waambieni watu kuwa wafuasi wake walikuja usiku na kuuiba mwili mlipokuwa mmesinzia. Gavana atakaposikia juu ya hili, tutazungumza naye ili msiadhibiwe.” Hivyo wale askari wakachukua pesa na kuwatii makuhani. Na jambo hili bado linasambaa miongoni mwa Wayahudi hata hivi leo. Wale wafuasi kumi na mmoja walikwenda Galilaya, kwenye mlima ambao Yesu aliwaambia waende. Wakiwa mlimani, wafuasi wale walimwona Yesu na wakamwabudu. Lakini baadhi ya wafuasi hawakuwa na uhakika kama alikuwa Yesu. Kisha Yesu akawajia na akasema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Hivyo nendeni ulimwenguni kote mkawafanye watu kuwa wafuasi wangu. Mkiwabatiza katika jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Wafundisheni kutii kila kitu nilichowaambia. Na tambueni hili: Niko pamoja nanyi daima. Na nitaendelea kuwa pamoja nanyi hata mwisho wa wakati.” Mwanzo wa Habari Njema za Yesu Masihi, Mwana wa Mungu, zilianza kama vile Nabii Isaya alivyosema zitaanza, aliandika, “Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako. Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.” “Kuna mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani: ‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana; nyoosheni njia kwa ajili yake.’” Naye Yohana akaja, akiwabatiza watu huko nyikani huku akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. Watu kutoka Yerusalemu na maeneo yote ya Uyahudi walikwenda kwa Yohana Mbatizaji; huko waliungama matendo yao mabaya kwake naye akawabatiza katika Mto Yordani. Huyo Yohana alivaa mavazi yaliyofumwa kutokana na manyoya ya ngamia. Naye alijifunga mkanda wa ngozi kuzunguka kiuno chake, na alikula nzige na asali mbichi. Yeye alitangaza yafuatayo: “Yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Mimi nawabatiza katika maji, lakini yeye huyo atawabatiza katika Roho Mtakatifu.” Ikatokea katika siku hizo Yesu alikuja toka Nazareti uliokuwa mji wa Galilaya akabatizwa na Yohana katika mto Yordani. Mara tu aliposimama kutoka ndani ya maji, Yesu aliona mpasuko ukitokea angani, akamwona Roho akishuka chini kuja kwake kama njiwa. Sauti ikasikika toka mbinguni, “Wewe ni mwanangu, ninayekupenda, napendezwa nawe sana.” Kisha baada ya kutokea mambo haya Roho Mtakatifu alimchukua Yesu na kumpeleka nyikani, naye akawa huko kwa siku arobaini, ambapo alijaribiwa na Shetani. Yesu alikuwa nyikani pamoja na wanyama wa porini, na malaika walimhudumia. Baada ya Yohana kuwekwa gerezani, Yesu akaja katika wilaya karibu na Ziwa Galilaya, huko aliwatangazia watu Habari Njema kutoka kwa Mungu. Akasema, “Wakati umefika. Ufalme wa Mungu umewafikia. Mbadili mioyo yenu na maisha yenu, na kuiamini habari njema!” Alipokuwa akitembea kando kando ya Ziwa Galilaya, Yesu alimwona Simoni na Andrea ndugu yake. Hao walikuwa wavuvi na walikuwa wakizitupa nyavu zao ziwani kukamata samaki. Yesu akawaambia, “njooni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa aina nyingine, nitawafundisha jinsi ya kukusanya watu badala ya samaki.” Mara moja, Simoni na Andrea wakaziacha nyavu zao na kumfuata. Kisha Yesu akaendelea mbele kidogo na akawaona ndugu wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na kaka yake Yohana. Yesu aliwaona wakiwa kwenye mashua wakiandaa nyavu zao za kuvulia samaki. Naye akawaita mara moja. Hivyo wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua na watu waliowaajiri na kumfuata Yesu. Kisha Yesu na wafuasi wake waliingia Kapernaumu. Siku ya Sabato Yesu aliingia katika sinagogi na akaanza kuwafundisha watu. Walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka. Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Naye mara alipiga kelele na kusema, “Unataka nini kwetu, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.” Lakini Yesu akamkemea na kumwambia, “Nyamaza kimya, na kisha umtoke ndani yake.” Ndipo roho yule mchafu akamfanya mtu yule atetemeke. Kisha akatoa sauti kubwa na kisha akamtoka. Kila mmoja akashangazwa sana kiasi cha kuwafanya waulizane, “Hii ni nini? Ni mafundisho ya aina mpya, na mtu yule anafundisha kwa mamlaka! Yeye huwapa amri pepo wachafu nao wanamtii!” Hivyo habari kuhusu Yesu zikaenea haraka katika eneo lote la Galilaya. Wakaondoka kutoka katika sinagogi na mara hiyo hiyo wakaenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. Mara Yesu alipoingia ndani ya nyumba watu wakamweleza kuwa mama mkwe wake Simoni alikuwa mgonjwa sana na alikuwa amepumzika kitandani kwa sababu alikuwa na homa. Yesu akasogea karibu na kitanda, akamshika mkono na kumsaidia kusimama juu. Ile homa ikamwacha, na yeye akaanza kuwahudumia. Ilipofika jioni, baada ya jua kuzama waliwaleta kwake watu wote waliokuwa wagonjwa na waliokaliwa na mashetani. Mji mzima ulikusanyika mlangoni pale. Naye akawaponya watu waliokuwa na magonjwa ya kila aina, na kufukuza mashetani wengi. Lakini yeye hakuyaruhusu mashetani kusema, kwa sababu yalimjua. Asubuhi na mapema, ilipokuwa giza na bado hakujapambazuka, Yesu aliamka na kutoka kwenye nyumba ile na kwenda mahali ili awe peke yake na kuomba. Lakini Simoni na wale wote waliokuwa pamoja naye waliondoka kwenda kumtafuta Yesu na walipompata, wakamwambia, “kila mmoja anakutafuta.” Lakini Yesu akawaambia, “Lazima twende kwenye miji mingine iliyo karibu na hapa, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hilo ndilo nililokuja kulifanya.” Hivyo Yesu alienda katika wilaya yote iliyoko mashariki mwa ziwa la Galilaya akihubiri Habari Njema katika masinagogi na kuwafungua watu kutoka katika nguvu za mashetani. Ikatokea mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea Yesu na kupiga magoti hadi chini akimwomba msaada. Mtu huyo mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwambia Yesu, “Kama utataka, wewe una uwezo wa kuniponya nikawa safi.” Aliposikia maneno hayo Yesu akakasirika. Lakini akamhurumia. Akautoa mkono wake na kumgusa mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi, na kumwambia, “Ninataka kukuponya. Upone!” Mara moja ugonjwa ule mbaya sana wa ngozi ulimwacha, naye akawa safi. Baada ya hayo Yesu akampa maonyo yenye nguvu na kumruhusu aende zake mara moja. Akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze, Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona kwa kuwa safi tena. Ukayafanye haya ili yawe uthibitisho kwa kila mmoja ya kwamba umeponywa.” Lakini mtu yule aliondoka hapo na kwenda zake, na huko alianza kuzungumza kwa uhuru kamili na kusambaza habari hizo. Matokeo yake ni kwamba Yesu asingeweza tena kuingia katika mji kwa wazi wazi. Ikamlazimu kukaa mahali ambapo hakuna watu. Hata hivyo watu walikuja toka miji yote na kumwendea huko. Siku chache baadaye Yesu alirudi Kapernaumu na habari zikaenea kuwa yupo nyumbani. Hivyo watu wengi walikusanyika kumsikiliza akifundisha na haikuwapo nafasi iliyobaki kabisa ndani ya nyumba, hata nje ya mlango. Yesu alipokuwa akifundisha, baadhi ya watu walimleta kwake mtu aliyepooza amwone. Mtu huyo alikuwa amebebwa na rafiki wanne. Watu hao hawakuweza kumfikisha mgonjwa kwa Yesu kwa sababu ya umati wa watu ulioijaza nyumba yote. Hivyo walipanda na kuondoa paa juu ya sehemu aliposimama Yesu. Baada ya kutoboa tundu darini kwenye paa, wakateremsha kirago alimokuwa amelala yule aliyepooza. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo wale waliomleta na yule mwenye kupooza, alimwambia, “Mtoto wangu, dhambi zako zimesamehewa.” Baadhi ya walimu wa sheria walikuwa wamekaa pale. Nao waliona kile alichokifanya Yesu na wakawaza miongoni mwa wenyewe, “Kwa nini mtu huyu anasema maneno kama hayo? Si anamtukana Mungu! Kwani hakuna awezaye kusamehe dhambi ila Mungu.” Mara moja Yesu alifahamu walichokuwa wakikifikiri wale walimu wa sheria, hivyo akawaambia, “Kwa nini mna maswali kama hayo mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza ‘Dhambi zako zimesamehewa,’ kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kirago chako na utembee’? Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina!” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kirago chako uende nyumbani!’” Yule mtu aliyepooza alisimama na bila kusita, akabeba kirago chake na akatoka nje ya nyumba wakati kila mmoja akiona. Matokeo yake ni kuwa wote walishangazwa na mambo hayo. Wakamsifu Mungu na kusema, “Hatujawahi kuona kitu kama hiki!” Mara nyingine tena Yesu akaelekea kandoni mwa ziwa, na watu wengi walikuwa wakimwendea, naye akawafundisha. Alipokuwa akitembea kando ya ufukwe wa ziwa, alimwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi katika mahala pake pa kukusanyia kodi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Hivyo Lawi akainuka na kumfuata. Baadaye Yesu na wafuasi wake wa karibu walikuwa wakila chakula cha jioni nyumbani kwa Lawi. Wakusanya kodi wengi na watu wengine wenye sifa mbaya nao wakamfuata Yesu. Hivyo wengi wao walikuwa wakila pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa pamoja na Mafarisayo walipomwona Yesu akila na wenye dhambi na wanaokusanya kodi, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Yesu anakula na wenye kukusanya kodi na watu wengine wenye dhambi?” Yesu alipolisikia hili akawaambia, “Wale walio wagonjwa ndio wanaomhitaji daktari si wale walio wazima wa afya. Mimi nimekuja kuwakaribisha wenye dhambi waje kwangu sikuja kwa ajili ya wale wanaotenda kila kitu kwa haki.” Siku moja wafuasi wa Yohana Mbatizaji na Mafarisayo walikuwa wanafunga. Baadhi ya watu walimjia Yesu na kumwuliza, “Mbona wafuasi wa Yohana na wafuasi wa Mafarisayo wanafunga, lakini kwa nini wanafunzi wako hawafungi.” Yesu akawajibu, “Katika sherehe ya arusi hutarajii marafiki wa bwana arusi wawe na huzuni wakati yeye mwenyewe yupo pamoja nao. Hakika hawatafunga ikiwa bwana arusi bado yuko pamoja nao. Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, na wakati huo ndipo watakapofunga. Hakuna anayeshona kiraka kipya cha nguo kwenye vazi la zamani. Ikiwa atafanya hivyo kiraka hicho kipya kitajikunjakunja na kulinyofoa vazi hilo zee nalo litachanika vibaya zaidi. Vivyo hivyo hakuna awekaye divai mpya ndani ya viriba vya zamani vilivyozeeka. Akifanya hivyo, divai ile itachacha na hewa yake itavipasua vibuyu hivyo vya ngozi na kuviharibu kabisa pamoja na divai yenyewe. Badala yake mtu anaweka divai mpya ndani ya vibuyu vipya vya ngozi vya kuwekea divai.” Ikatokea kwamba katika siku ya Sabato Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakipita katika mashamba ya nafaka. Wanafunzi wake walianza kuchuma masuke ya nafaka ile walipopita. Baadhi ya Mafarisayo walipoliona hilo wakamwambia Yesu, “Tazama, kwa nini wanafunzi wako wanafanya hivi? Ni kinyume cha sheria kuchuma masuke ya nafaka katika siku ya Sabato?” Yesu akajibu, “Hakika mmesoma kile alichofanya Daudi pale yeye pamoja na watu aliokuwa nao walipopata njaa na kuhitaji chakula. Ilikuwa wakati wa Abiathari Kuhani Mkuu. Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu na kula mkate uliotolewa kwa Bwana. Sheria ya Musa inasema ni makuhani peke yao ndio watakaoweza kuula mkate ule. Daudi aliwapa pia ule mkate mtakatifu watu waliokuwa pamoja naye.” Ndipo Yesu akawaambia mafarisayo, “Siku ya Sabato ilifanywa kwa faida ya watu. Watu hawakuumbwa ili watawaliwe na Sabato. Kwa hiyo Mwana wa Adamu ambaye ni Bwana juu ya kila kitu, pia ni Bwana juu ya siku ya Sabato.” Kwa mara nyingine tena Yesu alikwenda kwenye sinagogi. Huko alikuwepo mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa. Watu wengine walikuwa wakimwangalia Yesu kwa karibu sana. Walitaka kuona ikiwa angemponya mtu yule siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshitaki. Yesu akamwambia yule mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa, “Simama mbele ili kila mtu akuone.” Ndipo Yesu akawaambia, “Je, ni halali kutenda mema ama kutenda mabaya siku ya Sabato? Je, ni halali kuyaokoa maisha ya mtu fulani ama kuyapoteza?” Lakini wao walikaa kimya. Yesu akawatazama wote waliomzunguka kwa hasira lakini alihuzunika kwa sababu waliifanya mioyo yao kuwa migumu. Akamwambia mtu yule “nyosha mkono wako”, naye akaunyosha, na mkono wake ukapona. Kisha Mafarisayo wakaondoka na papo hapo wakaanza kupanga njama pamoja na Maherode kinyume cha Yesu kutafuta jinsi gani wanaweza kumuua. Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake hadi Ziwa Galilaya, na kundi kubwa la watu kutoka Galilaya likawafuata, pamoja na watu kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumea, na katika maeneo yote ng'ambo ya Mto Yordani na yale yanayozunguka Tiro na Sidoni. Lilikuwa kundi kubwa sana la watu. Wote walimjia Yesu kwa sababu walikuwa wamesikia mambo aliyokuwa anafanya. Kwa sababu ya kundi, aliwaambia wanafunzi wake, kumtayarishia mashua mdogo, ili kwamba wasiweze kumsonga na kumbana. Yesu alikuwa ameponya watu wengi. Hivyo wote wale waliokuwa na magonjwa waliendelea kujisogeza mbele kumwelekea ili wamguse. Kila mara pepo wachafu walipomwona Yesu, walianguka chini mbele yake, na kulia kwa sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini yeye aliwaamuru kila mara wasimwambie mtu yeyote yeye ni nani. Kisha Yesu akapanda juu kwenye vilima na akawaita baadhi ya wanafunzi wake, hasa wale aliowataka wajiunge naye pale. Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume. Aliwachagua ili waambatane pamoja naye, na kwamba aweze kuwatuma sehemu mbalimbali kuhubiri ujumbe wa neno la Mungu. Pia aliwapa mamlaka ya kufukuza mashetani toka kwa watu. Yafuatayo ni majina ya mitume kumi na wawili aliowateuwa Yesu: Simoni ambaye Yesu alimwita Petro, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu yake (ambao wote Yesu aliwaita Boanergesi), yaani “wana wa ngurumo yenye radi”, Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Thomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mzelote na Yuda Iskariote, ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu. Kisha Yesu akaenda nyumbani. Kwa mara nyingine tena umati wa watu ukakusanyika, kiasi kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakupata nafasi ya kula. Familia ya Yesu ilipoyasikia haya, walikwenda kumchukua kwa sababu watu walisema amerukwa na akili. Walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikuwa wanasema, “Yeye ana Beelzebuli ndani yake! Kwani anafukuza mashetani kwa nguvu ya mkuu wa mashetani!” Yesu akawaita na kuanza kuzungumza nao kwa kulinganisha: “Inawezekanaje Shetani ambaye ni roho mchafu kufukuza mashetani? Ikiwa basi ufalme utagawanyika katika sehemu mbili zinazopingana zenyewe kwa zenyewe, ufalme huo hautaendelea. Vivyo hivyo ufalme wa Shetani ukigawanyika naye akapigana dhidi ya pepo wake wabaya, basi huo utakuwa ndio mwisho wa ufalme wake. Pia ikiwa nyumba itapingana yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haitaweza kusalimika. Kwa hiyo ikiwa Shetani atajipinga mwenyewe na kugawanyika basi hataweza kuendelea na huo utakuwa mwisho wake. Hakika, hakuna anayeweza kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuzichukua mali zake bila kwanza kumfunga mtu huyo mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kuiba katika nyumba hiyo. Ninawaambia ukweli: Watu wanaweza kusamehewa dhambi zao zote na maneno yao yenye matusi kwa Mungu. Lakini yeyote atakayemtukana Roho Mtakatifu hatasamehewa kabisa. Kwa sababu mtu anayefanya hivyo atakuwa na hatia ya dhambi isiyosamehewa milele.” Yesu alisema haya kwa sababu walimu wa sheria walikuwa wanasema, “Yeye ana pepo mchafu ndani yake.” Kisha mama yake Yesu na nduguze wakaja. Wao walisimama nje na wakamtuma mtu aende kumwita ndani. Humo lilikuwepo kundi lililoketi kumzunguka, lakini wao wakamwambia, “Tazama! Mama yako, kaka zako na dada zako wako nje wanakusubiri.” Yesu akauliza, “Mama yangu ni nani na kaka zangu ni akina nani?” Yesu akawatazama wale walioketi kumzunguka na akasema “Hapa yupo mama yangu na wapo kaka zangu na dada zangu! Yeyote anayeyafanya mapenzi ya Mungu ndiye kaka yangu, dada yangu, na mama yangu.” Kwa mara nyingine Yesu akaanza kufundisha kando ya ziwa. Umati wa watu ukakusanyika kumzunguka, naye akapanda ndani ya mtumbwi ili akae na kufundisha huku mtumbwi ukielea. Yesu akawafundisha mambo mengi kwa simulizi zenye mafumbo. Katika mafundisho yake alisema: “Sikilizeni! Mkulima mmoja alitoka kwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akitupa na kuzisambaza mbegu hizo nyingine ikaanguka katika njia, na ndege wakaja na kuila. Mbegu nyingine ikaanguka juu ya uwanja wenye miamba, mahali ambapo hapakuwa na udongo wa kutosha. Hiyo mbegu ilichanua haraka kwani udongo ule haukuwa na kina cha kutosha. Lakini jua lilipochomoza, ule mmea uliungua na kwa sababu haukuwa na mizizi ya kutosha ulinyauka. Mbegu nyingine ilianguka kwenye magugu yenye miiba, na miiba ile ilikua na hatimaye kuibana sana na hivyo haikuzaa chochote. Mbegu nyingine ilianguka kwenye udongo mzuri, nayo ikaota, ikakua na kuzaa matunda; ikazaa mara thelathini, sitini na hata mia zaidi.” Kisha akasema, “Kila mwenye masikio mazuri ayasikie haya.” Yesu alipokuwa peke yake, wale waliomzunguka na wale kumi na wawili walimuuliza kuhusu mifano hiyo. Akawaambia, “Ni ninyi tu mliojaliwa kuzifahamu siri juu ya Ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walio nje nanyi mambo yote yatasemwa kwa simulizi zenye mafumbo, Ili kwamba, ‘japo watatazama sana hawataona, na kwamba japo watasikia sana hawataelewa; vinginevyo, wangegeuka na kusamehewa!’” Akawaambia, “Hamuelewi mfano huu? Sasa je mtaelewaje mfano wowote nitakaowapa? Mkulima ni badala ya yule anayepanda lile neno la Mungu. Watu wengine ni kama ile mbegu zilizoanguka juu ya njia pale ambapo neno la Mungu limepandwa. Baada ya kulisikia lile neno la Mungu, ndipo Shetani huja haraka na kuyaondoa yale mafundisho ya Mungu yaliyopandwa ndani yao. Watu wengine ni kama mbegu iliyopandwa kwenye eneo lenye mawe mengi. Wanapolisikia neno wanalipokea haraka kwa furaha. Lakini wao wenyewe wanakuwa bado hawajaliruhusu lizame zaidi katika maisha yao. Shida au mateso yanapotokea kwa sababu ya lile neno, kwa haraka sana wanaiacha imani. Watu wengine ni kama mbegu iliyopandwa katika miiba. Hawa ndio wale wanaolisikia neno, lakini mahangaiko ya maisha haya ya sasa, kuvutiwa na mali, na tamaa mbalimbali zingine huja na kulibana sana lile neno, nalo haliwezi kuwa na matokeo mazuri. Wengine ni kama mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri. Hawa ni wale wanaolisikia neno, na kulipokea na hivyo kuwa na matokeo mazuri; wengine kutoa thelathini, wengine sitini na wengine mia moja zaidi.” Yesu akawaambia, “Unapoileta taa ndani je unaiweka chini ya bakuli ama uvungu wa kitanda? Au unaileta ndani na kuiweka juu ya kitako cha taa? Kwani kila kilichofichika kitafunuliwa, na kila kilicho cha siri kitatokea kweupe kwenye mwanga. Yeyote mwenye masikio mazuri ni bora asikie.” Kisha akawaambia, “Zingatieni kwa makini kile mnachokisikia. Kwani jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa na kuzidi kuelewa. Kwa kuwa kila aliye na uelewa kidogo ataongezewa zaidi. Lakini wale wasiosikiliza kwa makini watapoteza hata ule uelewa mdogo walio nao.” Yesu akasema, “Hivi ndivyo Ufalme wa Mungu unavyofanana: Mtu mmoja alitoka kwenda kupanda mbegu zake katika udongo shambani. Usiku alienda kulala na asubuhi aliamka na zile mbegu zikiota na kukua; na hakujua jinsi gani hiyo ilifanyika. Ardhi yenyewe inatoa nafaka; kwanza hutoka shina, kisha kinafuata kichwa na mwishoni hutokea nafaka kamili katika kichwa. Nafaka ile inapokuwa imekomaa, basi mkulima huikata kwa fyekeo kwani wakati wa mavuno umekwishafika.” Yesu akasema, “Niufanananishe na kitu gani ufalme wa mbinguni? Au tutumie mfano gani kuuelezea? Ni kama mbegu ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko zote inapopandwa ardhini. Lakini inapokuwa imepandwa, inakua na kuwa kubwa sana kuliko mimea yote ya bustanini, na pia hubeba matawi makubwa, kiasi kwamba ndege wa angani wanaweza kupumzika katika kivuli chake.” Kwa mifano mingi kama hii aliendelea kuwafundisha kila kitu kwa kuzingatia uwezo wao wa kuelewa. Yesu hakusema kitu kwao bila kutumia mfano. Lakini alipokuwa peke yake pamoja na wanafunzi wake, alifafanua kila kitu kwao. Siku ile ilipofika jioni aliwaambia, “Hebu tuvuke kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa.” Kwa hiyo wakaliacha lile kundi. Wakamchukua pamoja nao alipokuwa amerudi katika mtumbwi. Wakati ule ule palikuwepo na mitumbwi mingi mingine ziwani. Dhoruba kubwa ikatokea na mawimbi yalikuwa yanakuja katika pembe zote za mtumbwi. Mtumbwi nao ulikaribia kujaa maji kabisa lakini Yesu alikuwa amelala nyuma ya mtumbwi akiegemea mto. Wakamwaamsha na kumwambia, “Mwalimu je wewe hujali kwamba tunazama?” Kisha akainuka, akaukemea upepo, na akaliamuru ziwa, “Nyamaza Kimya! Tulia!” Upepo ule ukatulia na ziwa nalo likatulia kabisa. Kisha akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Je! Bado hamna imani yoyote?” Lakini walikuwa na woga sana, na wakasemezana wao kwa wao, “Ni nani basi huyu ambaye hata upepo na ziwa vinamtii?” Wakafika ng'ambo ya ziwa, katika nchi walimoishi Wagerasi. Yesu alipotoka katika mashua ile ghafla, mtu mmoja aliyekuwa na roho chafu alitoka makaburini kuja kumlaki. Mtu huyu aliishi makaburini, na hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga hata kwa mnyororo, Watu walijaribu kila mara kumfunga kwa minyororo na vyuma kwenye miguu na mikono. Hata hivyo, aliweza kuivunja minyororo ile na pingu zile za vyuma wala hakuna aliyekuwa na nguvu za kutosha kumdhibiti. Kila mara usiku na mchana akiwa makaburini na kwenye milima alipiga kelele na kujikata kwa mawe. Alipomwona Yesu kutoka mbali, alimkimbilia, na kusujudu mbele yake. Kisha akalia kwa sauti kubwa na kusema, “Unataka nini kwangu, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Mkuu zaidi? Nakuomba uape mbele za Mungu kwamba hutanitesa.” Yule pepo alisema haya kwa sababu Yesu alikuwa anamwambia, “Mtoke huyo mtu, ewe pepo mchafu!” Ndipo Yesu akamwuliza yule mtu, “Jina lako nani?” Naye akamjibu, “Jina langu ni Jeshi, kwa sababu tuko wengi.” Yule pepo akamwomba Yesu tena na tena asiwaamuru kutoka katika eneo lile. Kulikuwepo kundi kubwa la nguruwe likila katika kilima. Wale pepo wakamwomba Yesu awatume waende katika lile kundi la nguruwe na kuliingia, Naye akawaruhusu. Kwa hiyo pepo wachafu walimtoka mtu yule na kuwaingia nguruwe. Kundi lile lilikuwa na idadi karibu ya elfu mbili, lilikimbia kuelekea kwenye kingo zenye mtelemko mkali na kutumbukia ziwani, ambamo walizama. Wale waliowachunga walikimbia. Wakatoa taarifa mjini na katika maeneo jirani ya mashambani. Watu wakaja kuona ni kitu gani kilichotokea. Watu hao wakamwendea Yesu. Nao wakamwona yule aliyekuwa na mashetani ameketi mahali pale, amevaa nguo na akiwa mwenye akili zake nzuri; huyu ni yule aliyekuwa amepagawa na jeshi la mashetani. Wakaogopa. Wale waliokuwa wameona hili waliwasimulia kile kilichomtokea mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani na kuhusu nguruwe wale. Nao wakamwomba Yesu aondoke katika eneo lile. Wakati Yesu akipanda katika mtumbwi, mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani alimwomba Yesu afuatane naye. Lakini Yesu hakumruhusu aende naye, isipokuwa alimwambia, “Nenda kwa watu wa kwenu, na uwaambie yote ambayo Bwana amekufanyia, na uwaambie jinsi alivyokuwa na huruma kwako.” Hivyo mtu yule aliondoka, na akaanza kuwaeleza watu katika Dekapoli mambo mengi ambayo Yesu amemtendea, na watu wote walistaajabu. Kisha, Yesu alivuka kurudi upande wa magharibi wa ziwa. Pale kundi kubwa la watu lilikusanyika kwake. Yeye alikuwa kando ya ziwa, na mmoja wa viongozi wa sinagogi, aliyeitwa Yairo, alifika pale. Naye alipomwona Yesu, alipiga magoti miguuni pake. Kisha akamwomba kwa msisitizo, akisema, “Binti yangu mdogo yu karibu kufa. Ninakuomba ufike na kumwekea mikono, ili kwamba apone na kuishi.” Hivyo Yesu alienda pamoja naye. Na kundi kubwa la watu lilimfuata; nao walikuwa wakimsonga pande zote kumzunguka. Alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa akitoka damu (kama ilivyo desturi ya wanawake kila mwezi) kila siku kwa miaka kumi na miwili. Huyu alikuwa ameteseka sana akiwa chini ya uangalizi wa madaktari wengi. Yeye alikuwa ametumia vyote alivyokuwa navyo. Hata hivyo hali yake iliendelea kuwa mbaya zaidi. Wakati aliposikia juu ya Yesu, alimwendea kwa nyuma akiwa katika kundi lile na kuligusa joho lake. Kwani alikuwa akijisemea mwenyewe, “Ikiwa nitagusa tu vazi lake, nitapona.” Mara moja chanzo cha kutoka kwake damu kikakauka, na akajisikia mwilini mwake kwamba amepona matatizo yake. Naye Yesu akatambua mara moja kwamba nguvu zilimtoka. Aligeuka nyuma na kuuliza “Nani aliyegusa mavazi yangu?” Wanafunzi wake wakamwambia, “Uliliona kundi likisukumana kukuzunguka, nawe unauliza, Nani aliyenigusa?” Lakini Yesu aliendelea kuangalia kumzunguka kuona ni nani aliyeyafanya haya. Yule Mwanamke akiwa anatetemeka kwa hofu akijua nini kilichotokea kwake, alikuja na kuanguka mbele yake, akamweleza ukweli wote. Kisha Yesu akamwambia, “Binti yangu imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, na uendelee kupona matatizo yako.” Wakati alipokuwa akizungumza haya watumishi walikuja kutoka nyumbani kwa afisa wa sinagogi. Nao wakamwambia yule afisa, “Binti yako amefariki kwa nini uendelee kumsumbua huyo mwalimu?” Lakini Yesu aliyasikia yale waliyokuwa wakisema, na akamwaambia yule afisa wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.” Naye hakumruhusu mtu yeyote kumfuata isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, nao wakaenda katika nyumba ya yule afisa wa sinagogi, na Yesu akaona vurugu na watu wakilia kwa sauti. Yesu aliingia ndani na kuwaambia, “Za nini vurugu zote hizi na vilio hivi? Mtoto hajafa; amelala tu.” Nao wakamcheka. Yeye aliwatoa nje watu wote, akamchukua baba na mama wa mtoto na wale waliokuwa pamoja naye, akaenda hadi pale alipokuwepo mtoto, akaushika mkono wa mtoto yule na kumwambia “ Talitha koum! ” (maana yake, “Msichana mdogo, ninakuambia amka usimame!”) Yule msichana aliinuka mara moja na kuanza kutembea mahali pale. Naye alikuwa na miaka kumi na miwili. Nao mara moja wakaelemewa na mshangao mkubwa. Yeye akawapa amri kuwa mtu yeyote asijue juu ya jambo hili. Kisha akawaambia wampatie msichana yule chakula ale. Yesu akaondoka pale, na kwenda katika mji wa kwao; na wanafunzi wake wakamfuata. Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sinagogi. Watu wengi walishangazwa walipomsikiliza. Wakasema, “Mtu huyu alipata wapi mambo haya? Alipata wapi hekima hii? Na anaifanyaje miujiza hii inayofanyika kwa mikono yake? Je, yeye si yule seremala? Je, yeye si mwana wa Maria? Je, yeye si kaka yake Yakobo, Yusufu, Yuda, na Simoni? Je, dada zake hawaishi hapa katika mji wetu?” Kulikuwa na vikwazo vilivyowazuia wasimkubali. Yesu akawaambia, “kila mtu humheshimu nabii isipokuwa watu wa mji wa kwao mwenyewe, jamaa zake mwenyewe na wale wa nyumbani mwake mwenyewe.” Yesu hakuweza kufanya miujiza ya aina yoyote pale, isipokuwa aliweka mikono juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. Naye akashangazwa na jinsi watu wa mji wa kwao mwenyewe walivyokosa kuwa na imani. Kisha Yesu alizunguka vijijini akiwafundisha watu. Akawaita kwake wanafunzi wake kumi na wawili, na akaanza kuwatuma wawili wawili. Akawapa uwezo wa kuwaweka huru watu kutoka pepo wachafu. Akawapa amri kuwa wasichukue kitu chochote kwa ajili ya safari yao isipokuwa fimbo; hawakupaswa kuchukua mkate, mfuko, hata kubeba fedha kwenye mikanda yao. Aliwaruhusu kuvaa makobazi lakini wasichukue kanzu ya pili. Naye akawambia, “ikiwa mtu atawapa mahali pa kuishi mkae katika nyumba hiyo kwa muda wote mtakapokuwa katika mji ule msihamehame kutoka nyumba moja hadi nyingine. Ikiwa hamtakaribishwa ama kusikilizwa katika mji wowote au mahali popote, kwa kuwaonya kunguteni mavumbi toka miguuni mwenu.” Kwa hiyo mitume wakatoka na kuhubiri ili watu watubu. Mitume wakafukuza mashetani wengi na kuwapaka mafuta ya mizeituni wagonjwa wengi na kuwaponya. Mfalme Herode alisikia habari hii kwani umaarufu wa Yesu ulikuwa umeenea mahali pote. Watu wengine walisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka wafu, ndiyo maana ana uwezo wa kufanya miujiza.” Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.” Wengine walisema, “Yeye ni nabii kama mmoja wa manabii wa zamani.” Lakini Herode aliyasikia haya na kusema, “Yohana, yule mtu niliyemkata kichwa, amefufuka kutoka kifo.” Kwa kuwa Herode mwenyewe alikuwa ametoa amri ya kumkamata Yohana na kumweka gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mkewe Filipo kaka yake ambaye Herode alikuwa amemwoa. Kwani Yohana alizidi kumwambia Herode, “Si halali kwako kisheria kumwoa mke wa kaka yako.” Herodia alikuwa na kisa na Yohana. Hivyo alitaka auwawe, lakini hakuweza kumshawishi Herode kumuua Yohana. Hii ni kwa sababu Herode alimhofu Yohana. Herode pia alifahamu ya kuwa Yohana alikuwa ni mtu mtakatifu na mwenye haki, hivyo akamlinda. Herode alimpomsikia Yohana, alisumbuka sana; lakini alifurahia kumsikiliza. Lakini muda maalumu ukafika; katika siku ya kuzaliwa kwake. Herode aliandaa sherehe ya chakula cha jioni kwa maafisa mashuhuri wa baraza lake, maafisa wake wa kijeshi, na watu maarufu wa Galilaya. Binti ya Herodia alipowasili ndani ya ukumbi alicheza na kumpendeza Herode na wageni aliowaalika katika sherehe hiyo. Mfalme Herode akamwambia yule msichana, “Uniombe chochote unachotaka, nami nitakupa.” Akamuahidi: “Nitakupa chochote utakachoniomba, hata nusu ya ufalme wangu!” Naye akatoka na kumwambia mama yake, “Niombe kitu gani?” Mama yake akasema, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.” Yule msichana mara moja aliharakisha kuingia ndani kwa mfalme na kuomba: “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji katika sinia.” Mfalme alisikitika sana. Lakini kwa sababu ya viapo vyake alivyovifanya mbele ya wageni wake chakulani hakutaka kumkatalia ombi lake. Kwa hiyo mfalme mara moja akamtuma mwenye kutekeleza hukumu za kifo akiwa na amri ya kukileta kichwa cha Yohana. Kisha akaenda kukikata kichwa cha Yohana, na kukileta katika sinia na kumpa yule msichana, na msichana akampa mama yake. Wanafunzi wa Yohana waliposikia haya walikuja na kuchukua mwili na kuuweka ndani ya kaburi. Mitume walikusanyika kumzunguka Yesu, na wakamweleza yote waliyofanya na kufundisha. Kisha Yesu akawaambia, “Njooni mnifuate peke yenu hadi mahali patulivu na palipo mbali na watu wengine ili mpumzike kidogo”, kwani pale walikuwepo watu wengi wakija na kutoka, nao hawakuwa na nafasi ya kula. Kwa hiyo wakaondoka na mtumbwi kuelekea mahali patulivu na mbali na watu wakiwa peke yao. Lakini watu wengi waliwaona wakiondoka na waliwafahamu wao ni kina nani; kwa hiyo walikimbilia pale kwa njia ya nchi kavu kutoka vitongoji vyote vilivyolizunguka eneo hilo wakafika kabla ya Yesu na wanafunzi wake. Alipotoka katika mashua, Yesu aliona kundi kubwa, na akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi. Kwa sasa ilikuwa imekwisha kuwa jioni sana. Kwa hiyo wanafunzi wake walimwijia na kusema, “Hapa ni mahali palipojitenga na sasa hivi saa zimeenda. Uruhusu watu waende zao, ili kwamba waende kwenye mashamba na vijiji vinavyozunguka na waweze kujinunulia kitu cha kula.” Lakini kwa kujibu aliwaambia, “Ninyi wenyewe wapeni kitu cha kula.” Wao Wakamwambia, “Je, twende kununua mikate yenye thamani ya mshahara wa mtu mmoja wa miezi minane na kuwapa wale?” Yesu akawambia, “Ni mikate mingapi mliyonayo? Nendeni mkaone.” Walienda kuhesabu, wakarudi kwa Yesu na kusema, “Tunayo mikate mitano na samaki wawili.” Kisha akawaagiza wakae chini kila mmoja kwenye majani mabichi kwa vikundi. Nao wakakaa kwa vikundi vya watu mia na mmoja na vya watu hamsini. Akachukua ile mikate mitano na samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akashukuru na akaimega. Akawapa wanafunzi wake ili wawape watu. Pia aligawanya samaki wawili miongoni mwao wote. Wakala na wote wakatosheka. Wakachukua mabaki ya vipande vya mikate na samaki na kujaza vikapu kumi na viwili. Na idadi ya wanaume waliokula ile mikate ilikuwa 5,000. Mara Yesu akawafanya wafuasi wake wapande kwenye mashua na wamtangulie kwenda Bethsaida upande wa pili wa ziwa, wakati yeye akiliacha lile kundi liondoke. Baada ya Yesu kuwaaga wale watu, alienda kwenye vilima kuomba. Ilipotimia jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu. Naye akawaona wanafunzi wake wakihangaika kupiga makasia, kwani upepo uliwapinga. Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi Yesu aliwaendea akitembea juu ya ziwa. Yeye akiwa karibu kuwapita, wanafunzi wake wakamwona akitembea juu ya ziwa, na wakafikiri kuwa alikuwa ni mzimu, ndipo walipopiga kelele. Kwa kuwa wote walimwona, na wakaogopa. Mara tu alizungumza nao na kuwaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Usiogope.” Kisha alipanda kwenye mtumbwi pamoja nao, na upepo ukatulia. Wakashangaa kabisa, kwa kuwa walikuwa bado hawajauelewa ule muujiza wa mikate. Kwani fahamu zao zilikuwa zimezibwa. Walipolivuka ziwa, walifika Genesareti na wakaifunga mashua. Walipotoka katika mashua, watu wakamtambua Yesu, Wakakimbia katika lile jimbo lote na kuanza kuwabeba wagonjwa katika machela na kuwapeleka pale waliposikia kuwa Yesu yupo. Na kila alipoenda vijijini, mijini na mashambani, waliwaweka wagonjwa kwenye masoko, na wakamsihi awaache waguse pindo la koti lake. Na wote walioligusa walipona. Mafarisayo na baadhi ya walimu wa Sheria waliokuja kutoka Yerusalemu walikusanyika mbele zake. Hao wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula chao kwa mikono michafu (yaani bila kuosha mikono yao). Kwani Mafarisayo na Wayahudi wengineo wote hawawezi kula isipokuwa wameosha mikono yao kwa njia maalumu, kulingana na desturi ya wazee. Na wanaporudi kutoka sokoni, hawali chakula kwanza mpaka wamenawa. Na zipo desturi nyingi wanazozishika, kama vile kuosha vikombe, magudulia na mitungi ya shaba. Kwa hiyo Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, badala yake wanakula chakula chao kwa mikono isiyo safi?” Yesu akawaambia, “Isaya alikuwa sahihi alipotoa unabii juu yenu enyi wanafiki, kama ilivyoandikwa: ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami. Ibada wanayonitolea haifai, kwa sababu wanawafundisha watu amri zilizotungwa na wanadamu kana kwamba ndizo itikadi zao.’ Mmezipuuza amri za Mungu, na mnashikilia desturi za binadamu.” Yesu akawaambia, “Ninyi ni wazuri katika kuzikataa amri za Mungu ili kuanzisha desturi yenu. Kwa mfano Musa alisema, ‘Mheshimu baba yako na mama yako,’ na yule mtu atakayesema maneno mabaya juu ya ‘mama au baba yake itampasa auwawe.’ Lakini ikiwa mtu atamwambia baba au mama yake, ‘Nilikuwa na kitu ambacho ningekupa kikusaidie, lakini nimeahidi kukitoa wakfu kwa Mungu, nacho sasa ni kurbani. ’ Kisha, anasema, hivyo hawezi kufanya kitu chochote kwa ajili ya kumsaidia baba au mama yake. Kwa hiyo unalifanya neno la Mungu kuwa batili kwa desturi mlizozirithishana. Na mnafanya mambo mengi mengine yanayofanana na hayo.” Yesu akaliita lile kundi kwake na kuwaambia, “Kila mmoja anisikilize na kunielewa. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu kinachoweza kumchafua kwa kumwingia. Lakini vitu vinavyotoka ndani ya mtu ndivyo vinavyomchafua.” *** Na alipoliacha lile kundi na kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza juu ya fumbo lile. Na akawaambia, “Hata nanyi hamuelewi pia? Je, hamuelewi ya kuwa hakuna kinachomwingia mtu kutoka nje kinachoweza kumchafua mtu? Kwa sababu hakiingii ndani ya moyo wake bali kinaenda tumboni mwake na kasha kinatoka na kwenda chooni.” Kwa kuyasema hayo alivifanya vyakula vyote kuwa safi. Na Yesu akasema, “Ni kile kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomchafua. Kwani mambo hayo yote mabaya hutoka ndani ya moyo wa mwanadamu; yaani mawazo mabaya na uasherati, wizi, mauaji, zinaa, ulafi, kufanya mabaya kwa watu, udanganyifu, kufanya uhuni, wivu, kutukana, kujivuna, na ujinga. Mambo haya yote yanatoka ndani ya mtu nayo ndiyo yanayomfanya asikubalike kwa Mungu.” Yesu akaondoka mahali pale na kuenda katika eneo lililozunguka Tiro. Aliingia katika nyumba na hakutaka mu yeyote ajue hilo, lakini hakuweza kufanya siri kuwepo kwake. Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo mchafu mara moja akasikia juu ya Yesu hivyo alimwijia na kuanguka chini yake. Mwanamke huyo alikuwa ni Mgiriki na siyo Myahudi, na alikuwa amezaliwa Foeniki ya Shamu. Yeye alimsihi amfukuze pepo yule kutoka kwa binti yake. Yesu akamwambia, “Kwanza waache watoto watosheke, kwani sio haki kuwanyanganya watoto mkate wao na kuwapa mbwa.” Lakini yeye akajibu, “Bwana hata mbwa walio chini ya meza wanakula mabaki ya chakula cha watoto.” Kisha Yesu akamwambia, “kwa majibu haya unaweza kwenda nyumbani kwa amani: pepo mbaya amekwisha mtoka binti yako.” Kwa hiyo akaenda nyumbani na akamkuta amelala akipumzika kitandani, na yule pepo tayari amekwisha mtoka. Yesu akarudi kutoka katika eneo kuzunguka jiji la Tiro na akapita katika jiji la Sidoni hadi Ziwa Galilaya akipita katika jimbo la Dekapoli. Pale watu wengine wakamletea mtu asiyeweza kusikia na tena aliyesema kwa shida. Nao wakamwomba Yesu amwekee mikono yake na kumponya. Yesu akamchukua pembeni, kutoka katika kundi, na akaweka vidole vyake ndani ya masikio yake. Kisha Yesu akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. Akaangalia juu mbinguni, akapumua na kumwambia “ Efatha ” yaani, “Funguka!” Mara masikio ya mtu yule yakafunguka, na ulimi wake ukawa huru, na akaanza kuzungumza, vizuri. Lakini kadiri jinsi alivyowaamuru wasimwambie mtu ndivyo walivyozidi kueneza habari hiyo. Na watu wakashangazwa kabisa na kusema, “Yesu amefanya kila kitu vyema. Kwani amewafanya wale wasiosikia kusikia na wasiosema kusema.” Wakati mwingine katika siku zile kundi kubwa la watu lilikusanyika na halikuwa na chakula. Yesu akawaita wanafunzi wake na kuwaambia, “Nawahurumia watu hawa, kwa sababu hata sasa wamekuwa nami kwa siku tatu, na hawana kitu cha kula.” Nikiwaacha waende majumbani mwao wakiwa na njaa, wataanguka njiani; na baadhi yao wametoka mbali. Wanafunzi wake wakamjibu, “Wapi mtu yeyote atapata chakula cha kutosha mahali hapa jangwani cha kuwalisha watu hawa?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakajibu, “Saba.” Kisha Yesu akaliagiza kundi la watu kuketi chini ardhini Akachukua mikate ile saba, akashukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake waigawe. Nao wakaigawa kwenye kundi. Kulikuwapo pia samaki wadogo wachache. Yesu akawabariki wale samaki na kuwaambia waigawe nayo pia. Watu walikula na kushiba. Wakakusanya vikapu saba vilivyojaa mabaki. Ilikuwa kama watu 4,000. Kisha Yesu akawaacha waende. Mara Yesu akapanda katika mashua na wanafunzi wake, na akafika katika wilaya ya Dalmanutha. Mafarisayo wakamwendea Yesu na kuanza kubishana naye. Ili kumjaribu wakamwomba ishara kutoka mbinguni. Yesu alihema kwa nguvu na kusema, “Kwa nini kizazi kinataka ishara? Ninawaambia ukweli: hakuna ishara itakayooneshwa kwa kizazi hiki.” Kisha Yesu akawaacha, akapanda tena katika mashua, na akaondoka kwenda upande wa pili wa ziwa. Wakati huo huo wanafunzi walikuwa wamesahau kuleta mikate yo yote, na hawakuwa na kitu kingine isipokuwa mkate mmoja. Yesu akawaonya, akasema, “Mwe mwangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ile ya Herode.” Nao wakaanza kujadiliana haya miongoni mwao: “Labda alisema hivi kwa sababu hatukuwa na mkate wowote.” Akijua walichokuwa wakikisema, akawaambia, “Kwa nini mnajadiliana juu ya kutopata mkate? Je! Bado hamwoni na kuelewa? Je! Mmezifunga akili zenu. Mnayo macho; Je! Hamwoni? Mnayo masikio; Je! Hamwezi kusikia? Mnakumbuka? Nilipomega na kugawa mikate mitano kwa watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?” Wakasema “Kumi na viwili”. “Nilipomega na kugawa mikate saba kwa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?” Wakasema “Saba”. Kisha akawaambia, “Bado hamwelewi?” Walipofika katika kijiji cha Bethsaida, baadhi ya watu walimleta asiyeona kwa Yesu, na kumsihi Yesu amguse. Yesu alimshika mkono yule asiyeona na kumtoa nje ya kijiji. Kisha Yesu alimtemea mate yule asiyeona kwenye macho yake, akaweka mkono wake juu ya asiyeona, na kumwuliza, “Je! Unaona kitu chochote?” Kipofu akatazama juu na kusema, “Ninaona watu; wanaonekana kama miti inayotembea.” Kisha Yesu akaweka mikono yake tena kwenye macho ya yule asiyeona. Naye akafumbua wazi macho yake yote. Kwani alipona kutokuona kwake na kuona kila kitu kwa uwazi. Kisha Yesu akamwambia arudi nyumbani, na pia akamwambia, “Usiingie kijijini.” Yesu na wanafunzi wake walikwenda kwenye vijiji vinavyozunguka Kaisaria Filipi. Wakiwa njiani aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?” Nao wakamjibu, “Yohana Mbatizaji. Wengine husema wewe ni Eliya. Na wengine husema wewe ni mmoja wa manabii.” Kisha akawauliza wao, “Na ninyi; Je! Mnasema mimi ni nani?” Petro akamjibu, “Wewe ni masihi.” Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote kuhusu yeye. Ndipo alianza kuwafundisha akisema: “Mwana wa Adamu lazima apate mateso mengi, na kukatataliwa na wazee, wakuu wa makuhani na walimu wa Sheria, na ni lazima atauawa na Kufufufuka baada ya siku ya tatu.” Yesu aliwaambia haya kwa uwazi bila kuwaficha. Baada ya mafundisho haya Petro alimchukua Yesu pembeni na kuanza kumkemea. Lakini Yesu aligeuka nyuma na kuwaangalia wanafunzi wake, na kumkemea Petro kwa kumwambia, “Shetani, toka mbele yangu! Huyajali yale anayoyajali Mungu bali yale wanayoyaona wanadamu kuwa ni muhimu.” Kisha Yesu akaliita kundi lote pamoja na wanafunzi wake kwake, akawaambia, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, lazima ajikane yeye mwenyewe, na ni lazima auchukue msalaba wake mwenyewe kisha anifuate. Kwa kuwa kila anayetaka kuusalimisha uhai wake, ataupoteza, na yeyote atakayeupoteza uhai wake kwa ajili yangu na kwa ajili ya injili atausalimisha. Itampa mtu manufaa gani akiupata ulimwengu wote kisha akaupoteza uhai wake? Mtu anaweza kuubadilisha uhai wake na kitu gani? Hiki ni kizazi chenye dhambi na kisichokuwa na uaminifu. Hivyo, mtu yeyote atakayenionea haya mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea haya mtu huyo siku ile atakaporudi katika utukufu wa Baba yake akiwa na malaika wake watakatifu.” Naye Yesu aliwaambia, “Ninawaambia Ukweli: baadhi yenu mnaosimama hapa mtauona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu kabla ya kufa kwenu.” Baada ya siku sita, Yesu akamchukua Petro, Yakobo na Yohana na kuwaongoza hadi mlima mrefu wakiwa peke yao tu. Na mwonekano wa Yesu ulibadilika mbele yao. Huko Yesu akabadilika sura nyingine akiwa mbele yao. Mavazi yake yakiwa na mng'ao, na meupe kabisa kuliko mtu anavyoweza kufua nguo kwa sabuni na kuitakatisha. Huko Eliya na Musa pia wakawatokea, na Yesu alizungumza na manabii hao wawili. Petro akafungua kinywa chake na kumwambia Yesu, “Mwalimu, ni vyema tupo hapa. Tufanye basi vibanda vitatu; moja kwa ajili yako, moja kwa ajili ya Musa na moja kwa ajili ya Eliya.” Petro aliyasema haya kwa sababu hakujua aseme nini, kwa sababu yeye na wenzake walikuwa wamepata hofu. Ndipo wingu likaja na kuwafunika wote kwa kivuli chake. Na sauti ikatoka mawinguni, ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa. Msikilizeni yeye.” Ndipo ghafula walipokuwa wakiangalia huku na huko, hawakuona mtu yeyote akiwa pamoja nao isipokuwa Yesu peke yake. Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote kile walichokiona mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka katika wafu. Hivyo hawakuwaeleza wengine juu ya jambo lile bali walijadiliana miongoni mwao wenyewe juu ya maana ya “kufufuka kutoka kwa wafu.” Wakamwuliza Yesu, “kwa nini walimu wa sheria wanasema Eliya lazima aje kwanza?” Yesu akawaambia, “Ndiyo, Eliya atakuja kwanza kuja kuyaweka mambo yote sawa kama jinsi yalivyokuwa hapo mwanzo. Lakini kwa nini imeandikwa juu ya Mwana wa Adamu ya kwamba itampasa kuteswa na kudhalilishwa? Lakini ninawaambia, Eliya amekuja, na walimtendea kila kitu walichotaka, kama vile ilivyoandikwa kuhusu yeye.” Wakati Yesu, Petro, Yakobo, na Yohana walipowafikia wanafunzi wengine, waliliona kundi kubwa la watu lililowazunguka na wakawaona walimu wa Sheria wakibishana nao. Mara tu watu wote walipomwona Yesu, walishangazwa, na wakakimbia kwenda kumsalimia. Akawauliza, “Mnabishana nao kitu gani?” Na mtu mmoja kundini alimjibu, “Mwalimu, nilimleta mwanangu kwako ili umponye. Yeye amefungwa na pepo mbaya anayemfanya asiweze kuzungumza. Na kila mara anapomshambulia humtupa chini ardhini. Naye hutokwa mapovu mdomoni na kusaga meno yake, huku akiwa mkakamavu. Nami niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze kutoka ndani yake, lakini hawakuweza.” Kisha Yesu akajibu na kuwaambia, “ninyi kizazi kisichoamini, kwa muda gani niwe pamoja nanyi? Kwa muda gani nitapaswa kuchukuliana nanyi? Mleteni huyo mvulana kwangu.” Wakamleta yule mvulana kwake. Na yule pepo alipomwona Yesu, kwa ghafula akamtingisha yule mvulana ambaye alianguka chini kwenye udongo, akivingirika na kutokwa povu mdomoni. Yesu akamwuliza babaye, “Kwa muda gani amekuwa katika hali hii?” Yule babaye akajibu akisema, “amekuwa katika hali hii tangu utoto. Mara nyingi anamtupa katika moto ama katika maji ili kumwua. Lakini ikiwa unaweza kufanya kitu chochote, uwe na huruma na utusaidie.” Yesu akamwambia, “Una maana gani kusema ‘ikiwa unaweza’? Kila kitu kinawezekana kwake yeye anayeamini.” Mara, babaye yule mvulana alilia kwa sauti kubwa na kusema, “Naamini! Nisaidie kutokuamini kwangu.” Yesu alipoona lile kundi likizidi kuwa kubwa, alimkemea yule pepo mchafu na kumwambia, “Wewe pepo uliyemfanya mvulana huyu asiweze kusikia na asiweze kusema, nakuamuru, utoke ndani yake, na usimwingie tena!” Na pepo yule alilia kwa sauti, akamtupa yule mvulana chini katika mishituko ya kutisha, kisha akatoka, naye akawa kama mtu aliyekufa, kiasi kwamba watu wengi wakadhani ya kuwa amekufa. Lakini Yesu akamshika yule mvulana mikononi, na kumwinua naye akasimama. Baada ya Yesu kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuuliza wakiwa peke yao, “Kwa nini sisi hatukuweza kumfukuza pepo yule?” Naye akawaambia, “Aina hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa maombi.” Wakaondoka mahali pale na kusafiri kupitia Galilaya. Yesu hakutaka mtu yeyote kujua walikuwa huko, alitaka kuwafundisha wanafunzi wake peke yake. Na Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kuwekwa mikononi mwa watu wengine, nao watamwua. Kisha siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.” Lakini hawakuuelewa usemi huu, na walikuwa wanaogopa kumuuliza zaidi. Kisha wakaja Kapernaumu. Na Yesu alipokuwa ndani ya nyumba aliwauliza, “Je, mlikuwa mnajidiliana nini njiani?” Lakini wao walinyamaza kimya, kwa sababu njiani walikuwa wamebishana juu ya nani kati yao alikuwa ni mkuu zaidi. Hivyo Yesu aliketi chini, akawaita wale kumi na mbili, na akawaambia, “Ikiwa yupo mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, inapasa basi awe wa mwisho kuliko wote na mtumishi wa wote.” Akamchukua mtoto mdogo mikononi mwake na kumsimamisha mbele yao. Akimkumbatia mtoto huyo, Yesu alisema, “Yeyote atakayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu hapa kwa sababu ya jina langu basi ananikaribisha na mimi pia. Yeyote anayenikubali mimi hanikubali mimi tu bali anamkubali pia yeye aliyenituma.” Yohana akamwambia Yesu, “Mwalimu tulimwona mtu akifukuza pepo kwa jina lako. Nasi tulijaribu kumzuia, kwa sababu hakuwa mmoja wetu.” Lakini Yesu akawaambia, “Msimzuie, kwa sababu hakuna atendaye miujiza kwa jina langu kisha mara baada ya hilo aseme maneno mabaya juu yangu. Yeye ambaye hapingani na sisi basi yuko pamoja na sisi. Yeyote anayewapa ninyi kikombe cha maji kwa sababu ninyi ni wake Kristo. Hakika ninawaambia ukweli kwamba, hatapoteza thawabu yake. Yeyote anayemsababisha mmoja wa hawa walio wadogo ambao wananiamini mimi kujikwaa na kuanguka, itakuwa bora kwake ikiwa atatupwa baharini huku amefungwa jiwe la kusagia shingoni mwake. Ikiwa mkono wako unakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa na mkono mmoja kuliko kuwa na mikono miwili na kuenda Jehanamu, ambako kuna moto usiozimika. *** Na ikiwa mguu wako utakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa mlemavu kuliko kuwa na miguu miwili na kutupwa Jehanamu. *** Na kama jicho lako litakusababisha ufanye dhambi, liondoe. Ni bora uingie katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja kuliko kuwa nayo macho mawili na kutupwa Jehanamu, ambapo waliomo watatafunwa na funza wasiokufa na kuchomwa na moto usiozimika kamwe. Kwa kuwa kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto. Chumvi ni njema. Lakini ikiwa chumvi itaharibika, utawezaje kuifanya chumvi tena? Muwe na chumvi miongoni mwenu na muishi kwa amani ninyi kwa ninyi.” Naye aliondoka mahali pale, na kufika katika nchi ya Uyahudi ng'ambo ya Mto Yordani. Na makundi ya watu wakamjia tena na kama alivyofanya daima aliwafundisha. Kisha baadhi ya Mafarisayo walimwendea na kumwuliza “Je, ni sahihi mtu kumtaliki mkewe?” Nao walimwuliza hivyo ili kumjaribu. Yesu akawajibu, “Musa aliwapa amri mfanye nini?” Wakasema, “Musa alimpa ruhusa mume kuandika hati ya kutangua ndoa na kisha kumtaliki mke wake.” Yesu akawaambia, “Musa aliwaandikia amri hii kwa sababu ninyi ni wakaidi na hamkutaka kuyapokea mafundisho ya Mungu. Lakini tangu mwanzo wa uumbaji wake Mungu ‘aliwaumba mwanaume na mwanamke’. ‘Basi kwa sababu ya hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, na kujiunga na mkewe. Na hao wawili wataungana pamoja na kuwa mwili mmoja.’ Nao si wawili tena bali ni mwili mmoja. Kwa hiyo, mtu yeyote asitenganishe kile ambacho Mungu amekiunganisha pamoja.” Walipokuwa ndani ya nyumba ile kwa mara nyingine, wanafunzi wake wakamwuliza Yesu juu ya jambo hili. Naye akawaambia, “yeyote atakayemtaliki mke wake na kuoa mwanamke mwingine, anazini kinyume cha mkewe. Na ikiwa mke atamtaliki mumewe na kuolewa na mume mwingine, basi naye anafanya zinaa.” Nao watu wakawaleta watoto wadogo kwa Yesu, ili aweze kuwawekea mikono na kuwabariki. Hata hivyo wanafunzi wake waliwakemea. Yesu alipoona hayo, alikasirika, na akawaambia, “Waruhusuni watoto hao waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu kama hao. Ninawaambia kweli, Yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyoupokea hataweza kuingia ndani yake.” Naye Yesu akawakumbatia watoto kifuani mwake na akaweka mikono yake juu yao na kuwabariki. Na alipokuwa ameanza safari, mtu mmoja alimkimbilia, akafika na kupiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Yesu akamwuliza, kwa nini unaniita mimi mwema? Hakuna aliye mwema isipokuwa Mungu peke yake. Je, unazijua amri: Usiue, usizini, usiibe, usitoe ushahidi wa uongo, usidanganye wengine, uwaheshimu baba na mama yako.” Naye akamwambia Yesu, “Mwalimu, nimeyatii hayo tangu ujana wangu.” Yesu akamwangalia. Naye akashikwa na upendo kwa mtu yule, na hivyo akamwambia, “umekosa kitu kimoja: Nenda ukaviuze vyote ulivyo navyo kisha ukawape walio maskini, nawe utakuwa umejitunzia hazina mbinguni. Kisha uje ukanifuate.” Yule mtu alisikitishwa sana na usemi huo, na akaondoka kwa huzuni kwa kuwa alikuwa na mali nyingi. Yesu aligeuka kuwatazama wanafunzi wake na kuwaambia wake, “Angalieni jinsi ilivyo vigumu sana kwa walio na mali nyingi kuingia katika ufalme wa Mungu.” Wanafunzi wake walistaajabishwa na maneno yale. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, ni vigumu sana kuuingia ufalme wa Mungu. Kwani ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuuingia ufalme wa Mungu.” Nao walistajaabu zaidi, na wakaambiana wao kwa wao, “Ni nani basi atakayeweza kuokolewa?” Huku akiwatazama, Yesu alisema, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, lakini kwa Mungu linawezekana, kwa sababu yote yanawezekana kwake Mungu.” Petro akaanza kumwambia, “Tazama! Tumeacha kila kitu tukakufuata.” Yesu akasema, “Nawaambieni kweli: Hakuna aliyeacha nyumba, kaka, dada, mama, baba, watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili ambaye hatapata malipo mara mia zaidi katika nyakati hizi; nyumba, kaka, dada, mama, watoto, na mashamba, pamoja na mateso; na uzima wa milele katika kizazi kinachokuja. Lakini wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho baadaye na wale walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza baadaye.” Walikuwa wote njiani wakipanda kuelekea Yerusalemu, na Yesu alikuwa akitembea mbele yao. Nao walisumbuka sana. Na wale waliowafuata walikuwa na hofu pia. Kwa mara nyingine Yesu akawachukua wale wanafunzi kumi na mbili pembeni, na akaanza kuwaeleza yale yatakayomtokea Yerusalemu. “Sikilizeni! Tunaelekea hadi Yerusalemu na Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria, nao watamtia hatiani na kumpa hukumu kifo, kisha watamtoa kwa wale wasio Wayahudi, Nao watamdhihaki, na watamtemea mate, na watamchapa kwa viboko vya ngozi, nao watamwua. Ndipo atafufuka baada ya siku ya tatu.” Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu, wakamwambia, “Mwalimu tunataka utufanyie kile tunachokuomba.” Yesu akawaambia, “Ni kitu gani mnachotaka niwafanyie?” Nao wakamwambia, “Uturuhusu tuketi pamoja nawe katika utukufu wako, mmoja wetu aketi kulia kwako na mwingine kushoto kwako.” Yesu akawaambia, “Hamjui mnachokiomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninachokinywea mimi? Au mnaweza kubatizwa ubatizo ninaobatizwa?” Wakamwambia, “Tunaweza.” Kisha Yesu akawaambia, “Mtakinywa kikombe cha mateso ninachokunywa mimi, na mtabatizwa ubatizo ninaobatizwa mimi. Lakini kuhusu kuketi kulia kwangu ama kushoto kwangu siyo mamlaka yangu kusema. Mungu ameandaa nafasi hizo kwa ajili ya wale aliowateuwa.” Wale wanafunzi kumi wengine walipoyasikia maombi haya, waliwakasirikia Yakobo na Yohana. Na Yesu akawaita wale wanafunzi kumi na kusema, “Mnajua kuwa miongoni mwa mataifa watawala huwa na mamlaka makubwa juu ya watu, na viongozi wenye nguvu huwakandamiza watu wao. Haipaswi kuwa hivyo miongoni mwenu. Kwani yeyote atakaye kuwa mkuu miongoni mwenu basi na awe mtumishi wenu. Yeyote anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima akubali kuwa mtumwa wenu wote. Kwani hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa bali alikuja kuwatumikia wengine na kuyatoa maisha yake ili kuwaweka huru wengi.” Kisha wakafika Yeriko. Yesu alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati wa watu, Bartimayo mwana wa Timayo, ombaomba asiyeona, alikuwa amekaa kando ya barabara. Aliposikia kwamba huyo alikuwa ni Yesu wa Nazareti, alianza kupiga kelele na kusema, “Yesu Mwana wa Daudi, unihurumie!” Na watu wengi walimkemea na kumwambia anyamaze kimya. Lakini yeye alipiga kelele kwa sauti kubwa zaidi na kusema, “Mwana wa Daudi, unihurumie!” Kwa hiyo Yesu akasimama na kusema, “Hebu mwiteni.” Nao wakamwita yule mtu asiyeona na kumweleza, “Jipe moyo mkuu! Inuka! Yesu anakuita.” Naye akalitupa joho lake, akaruka juu, na akamwendea Yesu. Naye Yesu akamwambia, “Unataka nikufanyie nini?” Yule mtu asiyeona akamwambia, “Mwalimu, nataka kuona tena.” Hivyo Yesu akamwambia, “Nenda! Imani yako imekuponya.” Na mara akaweza kuona tena, na akamfuata Yesu barabarani. Walipokaribia Yerusalemu walifika eneo la Bethfage na Bethania lililo karibu na Mlima wa Mizeituni, Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, na kuwaagiza, “Mwende katika kijiji kilichopo ngambo yenu kule, na mara tu mtakapoingia ndani yake mtakuta mwana punda amefungwa mahali na ambaye hajawahi kupandwa na mtu yeyote. Mfungueni na kisha mumlete hapa. Na mtu yeyote akiwauliza, ‘Kwa nini mnafanya hivi?’ ninyi mseme, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha kwenu mara moja.’” Hivyo wakaondoka, nao wakamkuta mwana punda huyo amefungwa katika mtaa wa wazi karibu na mlango. Wakamfungua. Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu na mahali pale wakawaambia, “Je, kwa nini mnamfungua mwana punda huyo?” Wanafunzi wake wakawaeleza yale walioambiwa na Yesu wayaeleze, nao wakawaacha waende zao. Kisha wakamleta mwana punda yule kwa Yesu na wakaweka mavazi yao ya ziada juu ya mwana punda, naye akampanda na kukaa juu yake. Watu wengi wakatandika makoti yao barabarani, na wengine wakatandika matawi waliyoyakata kwenye mashamba yaliyo jirani. Wote wale waliotangulia mbele na wale waliofuata walipiga kelele kwa shangwe, “‘Msifuni Mungu! Mungu ambariki yeye anayekuja katika Jina la Bwana!’ Mungu aubariki ufalme unaokuja, ufalme wa Daudi baba yetu! Msifuni Mungu juu mbinguni!” Ndipo Yesu aliingia Yerusalemu na kwenda hadi kwenye eneo la Hekalu akizunguka na kutazama kila kitu kilichokuwepo mahali hapo. Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda sana, aliondoka kwenda Bethania akiwa na wanafunzi wake kumi na wawili. Siku iliyofuata, walipokuwa wakiondoka Bethania, Yesu akawa na njaa. Na kutokea mbali akauona mti wa mtini umefunikwa kwa matawi yake mengi, hivyo akausogelea karibu ili kuona kama atakuta tunda lolote juu yake. Lakini alipoufikia hakukuta tunda lolote isipokuwa matawi tu kwani hayakuwa majira ya mitini kuwepo katika mti. Akauambia mtini ule, “Mtu yeyote asile matunda kutoka kwako kamwe milele!” Na wanafunzi wake waliyasikia hayo maneno. Walipofika Yerusalemu waliingia katika viwanja vya Hekalu. Yesu akaanza kuwafukuza nje wale waliokuwa wakifanya biashara ya kuuza na kununua katika eneo la Hekalu. Akapindua meza za wabadilishaji wa fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Pia hakumruhusu mtu yeyote abebe kitu chochote kukatiza eneo la Hekalu. Yesu akaanza kuwafundisha na kuwaeleza, “Je, haikuandikwa katika Maandiko kwamba: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ambapo watu wa mataifa yote wataleta maombi yao kwangu’? Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘mahali pa wezi kujificha.’ ” Na viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria waliyasikia haya, na hivyo wakaanza kutafuta njia ya kumuua. Kwani walimwogopa, kwa sababu watu wote walikuwa wamestaajabishwa na mafundisho yake. Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka Yerusalemu. Ilipofika asubuhi Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakitembea pamoja na wakauona ule mti wa mtini umekauka kuanzia kwenye mizizi yake. Petro akakumbuka yale Yesu aliyosema kwa mti huo na kumwambia, “Mwalimu, tazama! Mti ule wa mtini ulioulaani umenyauka kabisa.” Yesu akawajibu, “Mnapaswa kuweka imani yenu kwa Mungu. Nawaambia kweli: Yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ukajitupe katika bahari’; kama asipokuwa na mashaka moyoni mwake, Lakini akaamini kuwa kile anachokisema kitatokea, huyo atatendewa hayo. Kwa sababu hiyo nawaambia chochote mtakachoomba katika sala, muamini kwamba mmekipokea na haja mliyoiomba nayo itakuwa yenu, Na wakati wowote mnaposimama kuomba, mkiwa na neno lolote kinyume na mtu mwingine, mmsamehe mtu huyo. Na Baba yenu aliye mbinguni naye atawasamehe ninyi dhambi zenu.” *** Yesu na wanafunzi wake walirudi Yerusalemu. Na walipokuwa wakitembea ndani ya viwanja vya Hekalu, viongozi wa makuhani, walimu wa Sheria na wazee walimjia Yesu na kumwuliza, “Kwa mamlaka gani unafanya vitu hivi? Nani alikupa mamlaka ya kuvifanya?” Yesu akawaambia, “Nitawauliza swali, na mkinijibu, ndipo nitawaeleza kwa mamlaka gani ninafanya vitu hivi. Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni ama ulitoka kwa watu? Sasa mnijibu basi.” Walijadiliana wao kwa wao wakisema, “Tukisema ‘ulitoka mbinguni’, atasema, ‘Kwa nini basi hamumuamini?’ Lakini kama tukisema kuwa ubatizo wa Yohana ulitoka kwa wanadamu, watu watatukasirikia.” Viongozi waliwaogopa watu, kwani watu wote waliamini kuwa Yohana kweli alikuwa nabii. Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatufahamu.” Hivyo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.” Yesu alianza kuongea nao kwa simulizi zenye mafumbo: “Mtu mmoja alipanda mizabibu shambani. Akajenga ukuta kuizunguka, akachimba shimo kwa ajili ya kukamulia mizabibu na kisha alijenga mnara. Baadaye alilikodisha kwa baadhi ya wakulima na akaenda safari nchi ya mbali. Yalipotimia majira ya kuvuna, alimtuma mtumishi wake kwa wakulima wale, ili kukusanya sehemu yake ya matunda ya mzabibu. Lakini wakulima wale walimkamata mtumishi yule, wakampiga, na kumfukuza pasipo kumpa chochote. Kisha akamtuma mtumishi mwingine kwao. Huyu naye wakampiga kichwani na kumtendea mambo ya aibu. Yule mmiliki wa shamba la mzabibu akamtuma mtumishi mwingine, na wakulima wale wakamuua na yule pia. Baada ya hapo alituma wengi wengine. Wakulima wale waliwapiga baadhi yao na kuua wengine. Hata hivyo mwenye shamba yule bado alikuwa na mmoja wa kumtuma, mwanaye mpendwa. Alimtuma akiwa mtu wa mwisho. Akasema, ‘nina hakika watamheshimu mwanangu!’ Lakini wakulima wale walisemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye yule mrithi. Njooni tukamuue, na urithi utakuwa wetu!’ Kwa hiyo wakamchukua na kumuua, kisha wakautupa mwili wake nje ya shamba la mizabibu. Je! Mnadhani mwenye kumiliki lile shamba la mizabibu atafanya nini? Atakuja na kuwaua wakulima wale, na kukodisha shamba lile kwa watu wengine. Je! Hamjayasoma maandiko haya: ‘Jiwe ambalo wajenzi wamelikataa limekuwa jiwe kuu la msingi. Hii imefanywa na Bwana na ni ajabu kubwa kwetu kuona!’” Na viongozi wa kidini wakatafuta njia ya kumkamata Yesu, lakini waliogopa lile kundi la watu. Kwani walijua ya kwamba Yesu alikuwa ameisema simulizi ile yenye mafumbo ili kuwapinga. Kwa hiyo viongozi wa kidini wakamwacha na kuondoka. Viongozi wa Kidini wakamtumia baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili kumkamata kama akisema chochote kimakosa. Wale waliotumwa walifika na kumwambia, “Mwalimu tunajua, kwamba wewe ni mkweli, na tena hujali yale watu wanayoyafikiri kuhusu wewe, kwa sababu wewe hubabaishwi na wadhifa wa mtu. Lakini unafundisha ukweli wa njia ya Mungu. Tuambie ni haki kulipa kodi kwa Kaisari ama la? Je, tulipe au tusilipe?” Lakini Yesu aliutambua unafiki wao na akawaambia, “Kwa nini mnanijaribu hivi? Mniletee moja ya sarafu ya fedha mnazotumia ili niweze kuiangalia.” Hivyo wakamletea sarafu, naye akawauliza, “Je, sura hii na jina hili ni la nani?” Nao wakamwambia, “Ya Kaisari.” Ndipo Yesu alipowaambia, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake, na Mungu mpeni vilivyo vyake.” Wakastaajabu sana kwa hayo. Kisha Masadukayo wakamjia. (Hawa ni wale wanaosema hakuna ufufuo wa wafu.) Wakamwuliza, “Mwalimu, Musa alituandikia kwamba ikiwa kaka wa mtu atafariki na kumwacha mke asiye na watoto, Basi yule kaka lazima aoe mke yule wa nduguye na kuzaa naye watoto kwa ajili ya kaka yake aliyefariki. Palikuwepo na ndugu wa kiume saba. Wa kwanza alioa mke, naye alikufa bila kuacha mtoto yeyote. Wa pili naye akamwoa yule mke wa nduguye wa kwanza aliyeachwa naye akafa bila kuacha watoto wowote. Ndugu wa tatu pia alifanya vivyo hivyo. Ndugu wote wale saba walimwoa yule mwanamke na wote hawakupata watoto. Mwisho wa yote, yule mwanamke pia akafariki, Katika ufufuo, pale wafu watakapofufuka toka katika kifo, Je, yeye atakuwa mke wa nani? Kwani wote saba walikuwa naye kama mke wao.” Yesu akawaambia, “Hakika hii ndiyo sababu mmekosa sana: Hamyajui Maandiko wala uwezo wa Mungu. Kwa kuwa wafu wanapofufuka toka katika wafu, hawaoi wala kuolewa. Badala yake wanakuwa kama malaika walioko Mbinguni. Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, Je, hamjasoma katika kitabu cha Musa katika sura ile ya kichaka kinachoungua? Pale ndipo Mungu alipomwambia Musa, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.’ Yeye si Mungu wa waliokufa, bali wa wale wanaoishi. Hivyo ninyi mmekosa sana.” Mwalimu wa Sheria alifika naye aliwasikia wakijadiliana. Alipoona jinsi Yesu alivyowajibu vizuri sana, alimwuliza, “Je, amri ipi ni muhimu sana kuliko zote?” Yesu akajibu, “Muhimu sana ni hii: ‘Sikiliza, Israeli, Bwana Mungu wetu ni mmoja. Nawe unapaswa kumpenda Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa nafsi yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’ Amri ya pili ni hii: ‘mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ Hakuna amri nyingine kubwa kuliko hizi.” Na mwalimu wa Sheria akamwambia, “Umejibu vema kabisa mwalimu. Upo sahihi kusema kuwa Mungu ni mmoja, na hakuna mwingine ila yeye. Ni muhimu zaidi kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, kwa ufahamu wako wote, na kwa nguvu zako zote, na kumpenda jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe kuliko sadaka zote za kuteketezwa na matoleo tunayompa Mungu.” Yesu alipoona kwamba yule mtu amejibu kwa busara, alimwambia, “Wewe hauko mbali na Ufalme wa Mungu.” Baada ya hapo hakuwepo mtu mwingine aliyediriki kumwuliza maswali mengine zaidi. Yesu alipokuwa akifundisha katika mabaraza ya Hekalu, alisema, “Inawezekana vipi walimu wa Sheria kusema kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? Daudi mwenyewe kwa kupitia Roho Mtakatifu alisema, ‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu: Keti karibu nami upande wangu wa kuume, nami nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’ Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Itakuwaje tena Kristo awe yote Bwana na pia mwana wa Daudi?” Hapo lilikuwepo kundi kubwa la watu liliokuwa likimsikiliza kwa furaha. Katika mafundisho yake alisema, “Jihadharini na walimu wa Sheria.” Wao wanapenda kutembea huko na huko katika mavazi yanayopendeza huku wakipenda kusalimiwa masokoni, Hao wanapenda kukaa viti vya mbele katika masinagogi na kupewa sehemu muhimu zaidi za kukaa katika karamu za chakula. Hawa huwadanganya wajane ili wazichukue nyumba zao na wanasali sala ndefu ili kujionesha kwa watu. Watu hawa watapata hukumu iliyo kubwa zaidi. Yesu aliketi mahali kuvuka pale palipokuwepo na sanduku la matoleo, alitazama jinsi ambavyo watu walikuwa wakiweka sadaka zao sandukuni. Matajiri wengi waliweka fedha nyingi. Kisha mjane maskini alikuja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba, ambazo zilikuwa na thamani ndogo sana. Yesu aliwaita wanafunzi wake pamoja na kuwaambia, “Nawaambieni ukweli mjane huyu maskini ameweka sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kwamba ametoa zaidi ya matajiri wote wale.” Kwa kuwa wote walitoa kile cha ziada walichokuwa nacho. Lakini yeye katika umasikini wake, aliweka yote aliyokuwa nayo. Na hiyo ilikuwa fedha yote aliyokuwa nayo kutumia wa maisha yake. Yesu alikuwa akiondoka katika eneo la Hekalu na moja ya wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu, tazama mawe haya yanavyopendeza na jinsi majengo haya yanavyopendeza!” Yesu akamjibu, “Je, mnayaona majengo haya makubwa? Yote yatabomolewa. Kila jiwe litaporomoshwa hata chini. Hakuna jiwe lolote kati ya haya litakaloachwa mahali pake.” Naye alipokuwa ameketi juu ya Mlima wa Mizeituni upande wa pili kuvuka Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea walimwuliza wakiwa faragha, “Haya tuambie, ni lini mambo haya yatakapotokea? Ni ishara gani itakayoonesha ya kwamba yote yanakaribia kutimizwa?” Yesu akaanza kuwaeleza, “Muwe waangalifu mtu asije akawadanganya. Wengi watakuja huku wakilitumia Jina langu na kusema, ‘Mimi ndiye Masihi,’ nao watawadanganya wengi. Mtasikia juu ya vita vinavyopiganiwa na mtasikia habari juu ya vita vingine vinavyoanza. Hata hivyo msishtushwe. Mambo hayo lazima yatokee, kabla ule mwisho wenyewe kufika. Kwani taifa moja litapigana dhidi ya taifa lingine na ufalme mmoja utapigana dhidi ya ufalme mwingine. Yatatokea matetemeko mengi mahali pengi na kutakuwepo na njaa kali sehemu nyingi. Mambo haya yatakuwa ni mwanzo tu wa uchungu wa mama mzazi kabla ya mtoto kuzaliwa. Hivyo mjihadhari! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka mkahukumiwe kwa kuwa ninyi ni wanafunzi wangu. Watawapiga katika masinagogi yao. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na watawala. Nanyi mtawaeleza habari zangu. Kabla ya mwisho kufika, ni lazima kwanza habari Njema itangazwe kwa mataifa yote. Wakati wowote watakapowakamata na kuwashitaki, msiwe na wasiwasi kujiandaa kwa yale mtakayoyasema, lakini myaseme yale mtakayopewa saa ile ile, kwa kuwa si ninyi mnaozungumza; bali, ni Roho Mtakatifu anayezungumza. Na ndugu atamsaliti nduguye hata kuuawa, na baba atamsaliti mwanawe. Watoto nao watawaasi wazazi wao na hata kuwatoa wauawe. Nanyi mtachukiwa na wote kwa sababu yangu. Lakini yeyote atakayevumilia hadi mwisho ataokoka. Wakati mtakapoliona chukizo la uharibifu likisimama mahali pasipotakiwa lisimame.” (Msomaji aelewe hii ina maana gani? ) “Kisha wale waliopo katika Uyahudi wakimbilie milimani. Ikiwa mtu yupo katika paa la nyumba yake, asishuke chini na kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu chochote. Ikiwa mtu yupo shambani asirudi kuchukua vazi lake. Wakati huo itakuwa hatari kwa wanawake walio waja wazito na wale wenye watoto wachanga. Ombeni kwamba haya yasitokee wakati wa majira ya baridi. Kwa kuwa taabu itakayotokea katika siku hizo itakuwa ile ambayo haijawahi kutokea tangu mwanzo pale Mungu alipoumba dunia hadi sasa. Na hakitatokea tena kitu kama hicho. Kama Bwana asingelifupisha muda huo, hakuna ambaye angenusurika. Lakini yeye amefupisha siku hizo kwa ajili ya watu wale aliowateuwa. Ikiwa mtu atawaambia, ‘Tazama, Kristo ni huyu hapa!’ ama ‘Ni yule pale!’ Usiliamini hilo. Kwani Makristo wa uongo na manabii wa uongo watatokea, nao watafanya ishara na miujiza kuwadanganya watu ikiwezekana hata wale ambao Mungu amewachagua. Kwa hiyo mjihadhari nimewaonya juu ya mambo haya kabla hayajatokea. Lakini katika siku hizo, baada ya kipindi cha dhiki, ‘Jua litatiwa giza, mwezi hautatoa mwanga, nyota zitaanguka kutoka angani, na mbingu yote itatikisika.’ Ndipo watu watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na nguvu kubwa na utukufu. Baada ya hapo Mwana wa Adamu atawatuma malaika, na atawakusanya wateule wake kutoka kila upande wa dunia. Jifunzeni somo hili kutoka katika mti wa mtini: Matawi yake yanaponyauka na kubeba majani, unajua kwamba kiangazi kimekaribia. Vivyo hivyo, unapoona mambo haya yanaanza kutokea unajua kwamba muda umekaribia na umeshafika mlangoni. Ninawaambieni ukweli: Kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo haya yote hayajatokea. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. Hakuna anayejua wakiwemo malaika wa mbinguni ama Mwana bali baba peke yake lini siku au saa ile itakapowadia. Mjihadhari; Kesheni! Kwani hamjui lini muda huo utafika. Ni kama mtu anayeenda safarini na kabla ya kuondoka huiacha nyumba yake mikononi mwa watumishi wake. Kabla ya kuiacha nyumba yake anawaweka watumishi wake kusimamia kila mmoja akiwa na kazi yake maalumu. Kisha atamwamuru mlinzi mlangoni awe macho. Vivyo hivyo ni lazima mjihadhari, kwa sababu hamjui ni muda gani mkuu wa nyumba atakuja; hamjui kama atakuja jioni, usiku wa manane, wakati jogoo anawika, au alfajiri. Ikiwa atakuja ghafula, basi asiwakute mmelala. Ninachowaambia, namwambia kila mmoja: ‘muwe tayari.’” Ilikuwa yapata siku mbili kabla ya Sikukuu ya Pasaka na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Wakuu wa makuhani na walimu wa Sheria walikuwa wakitafuta njia, kwa ujanja fulani, ya kumkamata na kumuua Yesu. Kwani walikuwa wakisema “tusifanye hivi wakati wa sherehe, ama sivyo watu watafanya fujo.” Yesu alikuwa Bethania, katika nyumba ya Simoni mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Wakati ameketi mezani mwanamke mmoja alimwijia. Naye alikuwa na gudulia la mawe lililojaa manukato ya bei ghali yaliyotengenezwa kwa nardo safi. Mwanamke huyo alilifungua gudulia lile kwa kulivunja na kumwagia Yesu manukato kichwani mwake. Baadhi ya watu waliokuwa pale walikasirika na kulalamika miongoni mwao, “Kwa nini kuwepo na ufujaji wa manukato namna hii? Gharama yake ni sawa na mshahara wa mwaka mzima. Manukato haya yangeweza kuuzwa na fedha hiyo kupewa walio maskini.” Kisha wakamkosoa yule mwanamke kwa hasira kwa jambo alilolifanya. “Lakini Yesu alisema mwacheni peke yake. Kwa nini mnamsumbua? Yeye amenifanyia kitendo chema. Kwani siku zote mnao maskini pamoja nanyi na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini hamtakuwa pamoja nami siku zote. Yeye amefanya kile alichokiweza kufanya. Ameumwagia manukato mwili wangu kabla ya wakati kuuandaa kwa ajili ya maziko. Ninawaambia kweli: Popote injili itakapohubiriwa ulimwenguni, kile alichokifanya kitasimuliwa kwa kumkumbuka.” Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na mbili, aliwaendea viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao. Nao walifurahi kusikia hivyo, na wakaahidi kumpa fedha. Kwa hiyo Yuda akaanza kutafuta wakati unaofaa wa kumsaliti. Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, ambapo kila mara mwana kondoo alitolewa sadaka kwa ajili ya Pasaka. Wanafunzi wa Yesu wakamwendea na kumwuliza, “Ni wapi unapotaka tuende kukuandalia ili uweze kuila Karamu ya Pasaka?” Hivyo Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, naye akawaeleza, “ingieni mjini, na mtakutana na mtu mmoja aliyebeba gudulia la maji. Mfuateni, popote pale atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba ile, ‘mwalimu anasema, utuonyeshe chumba ambacho yeye na wanafunzi wake wanaweza kuila Karamu ya Pasaka.’ Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, klichoandaliwa tayari kwa ajili yetu. Basi mtuandalie chakula pale.” Wanafunzi wa Yesu waliondoka na kuelekea mjini. Huko walikuta kila kitu kama vile Yesu alivyowaeleza Hivyo, waliandaa mlo wa Pasaka. Wakati wa jioni Yesu alienda pamoja na wanafunzi wake kumi na mbili katika nyumba ile. Wote walipokuwa wameketi mezani wakila, Yesu akasema, “Mniamini ninapowambia kwamba mmoja wenu, yule anayekula nami sasa atanitoa kwa maadui zangu.” Wanafunzi walihuzunika sana kusikia jambo hili. Kila mmoja akamwambia Yesu, “Hakika siyo mimi?” Akawaambia, “Ni mmoja wa wale kumi na mbili; na ni yule atakayechovya mkate katika bakuli pamoja nami. Mwana wa Adamu atakiendea kifo chake kama ilivyoandikwa juu yake. Lakini itakuwa ya kutisha namna gani kwa mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu anasalitiwa. Itakuwa bora mtu huyu asingelikuwa amezaliwa.” Na walipokuwa wakila Yesu aliuchukua mkate, akamshukuru Mungu kwa huo. Akamega vipande, akawapa wanafunzi wake, na kusema, “Chukueni na mle mkate huu. Ni mwili wangu.” Kisha akakichukua kikombe chenye divai, akamshukuru Mungu kwa hicho, akawapa. Wote wakanywa toka kile kikombe. Kisha akasema, “Kinywaji hiki ni damu yangu ambayo kwayo Mungu anafanya agano na watu wake. Damu yangu inamwagika kwa manufaa ya watu wengi. Ninawaambia kweli sitakunywa diva tena mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya katika Ufalme wa Mungu.” Na wao wakaimba mwimbo wa sifa na kutoka na kuelekea kwenye Mlima wa Miti ya Mizeituni. Yesu akawaambia, “Nyote mtaniacha, kwani imeandikwa, ‘Nitamuua mchungaji, na kondoo watatawanyika.’ Lakini baada ya kuuawa, nitafufuka kutoka kwa wafu. Kisha nitaenda Galilaya. Nitakuwa pale kabla ninyi hamjafika.” Lakini Petro akamwambia, “Hata kama wengine wote watapoteza imani yao, mimi sitapoteza imani yangu.” Ndipo Yesu akamjibu kusema, “Ukweli ni kwamba, usiku wa leo utasema kuwa hunijui. Utasema hivyo mara tatu kabla ya jogoo kuwika mara mbili.” Petro akasema kwa kusisitiza zaidi, “Hata kama itanipasa kufa nawe, sitasema kuwa sikujui.” Na wengine wakasema hivyo. Kisha wakafika mahali palipoitwa Gethsemane. Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati ninaomba.” Naye Yesu akamchukua Petro, Yakobo, na Yohana pamoja naye, naye akaanza kusumbuka sana. Akawaambia, “Nina huzuni sana na ninafikiri inaweza kuniua. Kaeni hapa, na mjihadhari.” Akiendelea mbele kidogo, alianguka chini, na akaomba ikiwezekana angeiepuka saa ya mateso. Akasema, “ Aba, yaani Baba, vyote vinawezekana kwako wewe. Hebu kiondoe kikombe hiki kutoka kwangu, Lakini usifanye kama ninavyopenda mimi, lakini kama unavyopenda wewe.” Kisha Yesu akaja na kuwakuta wamelala, na akamwuliza Petro, “Simoni, je umelala? Je, hukuweza kukaa macho kwa muda wa saa moja tu? Kaeni macho na kuomba, ili msije mkaingia majaribuni. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.” Yesu akaondoka kwenda kuomba tena, akilisema jambo lile lile. Kisha akarudi tena na kuwakuta wamelala, kwani macho yao yalikuwa yamechoka. Wao hawakujua la kusema kwake. Alirudi mara ya tatu na kuwaambia, “Je, bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imefika. Mwana wa Adamu atasalitiwa mikononi mwa watenda dhambi. Amkeni! Twendeni! Tazama! Yule atakayenisaliti amekaribia.” Mara moja, wakati Yesu akali akizungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na mbili, alitokea. Pamoja naye walikuwa kundi kubwa la watu waliokuwa na majambia na marungu wakitoka kwa viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na wazee. Msaliti alikuwa tayari amewapa ishara: “Yule ambaye nitambusu ndiye mwenyewe. Mkamateni, mlindeni na muwe waangalifu mnapomwondoa.” Mara tu Yuda alipowasili, alimwendea Yesu. Alipomkaribia alisema, “Mwalimu!” Kisha akambusu. Ndipo walipomkamata na kumshikilia. Mmoja wa wale waliosimama naye karibu akautoa upanga wake alani, akampiga nao mtumishi wa kuhani mkuu na kulikata sikio lake. Kisha Yesu akawaambia, “Je, mlikuja kunikamata kwa upanga na marungu, kama vile mimi nimekuwa jambazi? Kila siku nilikuwa nanyi, nikifundisha Hekaluni na hamkujaribu kunikamata wakati huo. Lakini Maandiko lazima yatimie.” Wafuasi wake wote walimwacha na kumkimbia. Miongoni mwa watu waliomfuata Yesu alikuwa kijana mmoja aliyevaa kipande cha nguo. Watu walipotaka kumkamata alikiacha kile kipande cha nguo mikononi mwao na kukimbia akiwa uchi. Nao wakamwongoza Yesu kumpeleka kwa kuhani mkuu, na viongozi wote wa makuhani, wazee, na walimu wa Sheria walikutanika. Petro akamfuata Yesu kwa mbali kidogo hadi ndani ya baraza la nyumba ya kuhani mkuu. Petro alikuwa ameketi na wale walinzi akijipasha joto na moto walioukoka. Viongozi wa makuhani na Baraza lote la Wayahudi walikuwa wakitafuta ushahidi dhidi ya Yesu wa kuweza kumhukumu kifo, lakini hawakupata kitu chochote. Watu wengi walikuja na kutoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini wote walisema vitu tofauti. Ushahidi wao ulipingana. Kisha wengine walisimama na kushuhudia kinyume chake kwa uongo, wakisema, “Tulimsikia mtu huyu akisema, ‘Nitaliharibu Hekalu hili lililotengenezwa kwa mikono ya wanadamu, na kwa siku tatu nitajenga lingine ambalo halikujengwa kwa mikono.’” Lakini hata katika ushahidi wao huu hawakukubaliana. Kisha kuhani mkuu akasimama mbele yao na akamwuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Nini ushahidi huu ambao watu wanaleta dhidi yako?” Lakini Yesu alinyamaza kimya na hakutoa jibu lolote. Kwa mara nyingine kuhani mkuu akamwuliza, “Je, wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu anayesifiwa?” Yesu akasema, “Mimi ndiye. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye uweza wote akija pamoja na mawingu ya mbinguni.” Kuhani mkuu alichana mavazi yake na kusema, “Tuna haja gani ya kuleta mashahidi zaidi? Ninyi wote mmesikia akimtolea Mungu matusi.” Wote walimhukumu na kumwona kwa anastahili kifo. Na wengine walianza kutema mate, na kufunika uso wake, na kumpiga, na kumwambia, “Uwe nabii na utuambie nani aliyekupiga.” Kisha wale walinzi walimchukua na kuendelea kumpiga. Wakati Petro alipokuwa bado barazani, mtumishi wa kike wa kuhani mkuu alifika pale. Alipomwona Petro akijipasha moto, alimkazia macho na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.” Lakini Petro alisema, “Hii si kweli, mie sifahamu wala kuelewa kile unachokisema.” Baada ya hapo Petro alitoka na kwenda barazani na hapo hapo jogoo akawika. Yule mtumishi wa kike alipomwona alirudia tena kuwaeleza wale waliokuwa wamesimama pale, “Mtu huyu ni mmoja wao!” Kwa mara nyingine tena Petro alikataa. Baada ya muda mfupi wale waliokuwa wamesimama pale wakarudia tena kumwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa sababu wewe pia ni Mgalilaya.” Petro akaanza kutoa maneno makali na kusema, “Naapa kwa Mungu, simjui mtu huyu mnayemzungumzia!” Mara jogoo akawika kwa mara ya pili, na Petro akakumbuka lile neno la Yesu alilomwambia: “Kabla kogoo hajawika mara ya pili utanikana mara tatu.” Naye akavunjika moyo na kuanza kulia. Asubuhi na mapema, Mara tu ilipofika asubuhi viongozi wa makuhani, viongozi wazee wa Kiyahudi, walimu wa sheria, na baraza kuu lote la Wayahudi liliamua jambo la kufanya kwa Yesu. Walimfunga Yesu, wakamwondoa pale, na wakamkabidhi kwa Pilato. Na Pilato akamwuliza: “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu “Hayo ni maneno yako mwenyewe.” Na viongozi wa makuhani wakamshitaki Yesu kwa mambo mengi. Kwa hiyo Pilato akamwuliza Yesu swali lingine. Akasema, “Wewe hata kujibu hujibu? Angalia una mashitaka mengi wanayokuletea!” Lakini Yesu hakujibu kitu chochote, na Pilato akastaajabu. Kila mwaka wakati wa Sherehe ya Pasaka Pilato atamweka huru mfungwa mmoja atakayechaguliwa na watu. Mtu mmoja aliyeitwa Baraba alikuwa gerezani amefungwa pamoja na waasi. Watu hawa walifanya mauaji wakati wa fujo. Watu walikuja Kwa Pilato na kumwomba amweke huru mfungwa kama alivyofanya siku zote. Yeye akawauliza, “Je, mnataka nimwache huru mfalme wa Wayahudi?” Pilato alilisema hili kwa sababu alijua kuwa viongozi wa makuhani walimleta kwake kwa ajili ya wivu tu. Lakini wale viongozi wa makuhani walimchochea amwache Baraba badala ya Yesu. Lakini Pilato akawauliza watu tena, “Kwa hiyo nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?” Wakapiga kelele “Muue kwenye msalaba.” Lakini Pilato akawauliza, “Kwa nini? Je, amefanya kosa gani?” Lakini wote wakapiga kelele zaidi, “Muue kwenye msalaba!” Pilato alitaka kuwaridhisha watu, kwa hiyo alimweka huru Baraba kwa ajili yao. Akaamuru maaskari wampige Yesu viboko na kisha akamtoa kwao ili akauawe kwenye msalaba. Maaskari wakamwongoza Yesu hadi ndani ya baraza la jumba la gavana (lililojulikana kama Praitorio). Huko wakakiita pamoja kikosi cha maaskari. Wakamvalisha Yesu joho la zambarau na wakafuma taji ya miiba na kumvisha kichwani. Kisha wakaanza kumpigia saluti wakisema: “Heshima kwa Mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga tena na tena kichwani kwa fimbo na wakamtemea mate. Kisha wakapiga magoti mbele yake na kujifanya wanampa heshima kama mfalme. Walipomaliza kumkejeli walimvua joho lile la kizambarau, na kumvisha mavazi yake mwenyewe. Baada ya hapo wakamtoa nje ili waweze kumsulubisha. Wakiwa njiani walikutana na mtu kutoka Kirenio aliyeitwa Simoni, akitoka vijijini kuja mjini. Yeye alikuwa baba yake Iskanda na Rufo. Wale wanajeshi wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. Wakamleta Yesu hadi mahali palipoitwa Golgotha (Yaani Mahali pa Fuvu la Kichwa) Nao wakampa divai iliyochanganywa na siki, lakini yeye alikataa kuinywa. Pale wakampigilia kwa misumari msalabani. Wakagawana mavazi yake miongoni mwao nao wakayapigia kura ili kuona kila mtu atapata nini. Ilikuwa saa tatu asubuhi walipompigilia kwa misumari msalabani. Ilani ya mashtaka dhidi yake ilikuwa na maandishi haya juu yake: “MFALME WA WAYAHUDI.” Hapo waliwapigilia msalabani wahalifu wawili pembeni mwa Yesu, mmoja kushoto kwake na mwingine kuume kwake. *** Watu waliopita mahali pale walimtukana. Walitikisa vichwa vyao na kusema, “Haya! Wewe ndiye yule awezaye kuliharibu hekalu na kulijenga tena kwa siku tatu. Hebu shuka msalabani na uyaokoe maisha yako.” Kwa njia hiyo hiyo, viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria walimfanyia dhihaka na wakasema wao kwa wao, “Aliwaokoa wengine lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Ikiwa yeye kweli ni Masihi Mfalme wa Israeli, iinampasa ashuke sasa toka msalabani, tukiliona hilo nasi tutamwamini.” Wale wahalifu waliokuwa katika misalaba ile mingine pembeni waliosulubiwa pamoja naye nao walimtukana. Ilipofika saa sita mchana giza ilifunika nchi yote. Giza liliendelea hadi saa tisa. Mnamo saa tisa Yesu alipiga kelele kwa sauti na kusema, “ Eloi, Eloi, lema sabakthani? ” maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Na baadhi ya wale waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hivi, walisema, “sikilizeni anamwita Eliya.” Mtu mmoja alikimbia na kujaza sifongo kwenye siki, akaliweka kwenye ufito, na akampa Yesu anywe akisema, “Subiri! Tuone ikiwa Eliya atashuka na kumshusha chini.” Yesu akalia kwa sauti kubwa na kisha akafa. Hapo pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili kutoka juu hadi chini. Yule afisa wa jeshi aliyekuwa amesimama pale mbele na kuona jinsi Yesu alivyokufa. Afisa huyu alisema, “mtu huyu hakika alikuwa mwana wa Mungu!” Baadhi ya wanawake walikuwa wakiangalia mambo haya toka mbali. Miongoni mwao alikuwapo Maria Magdalena, Salome, na Maria mama yake Yakobo na Yose. Wanawake hawa ni wale waliomfuata Yesu huko Galilaya na kumhudumia. Wanawake wengi wengine waliofuatana naye kuja Yerusalemu walikuwapo pale pia. Siku hii ilikuwa ni Siku ya Maandalizi ya Sabato. (Maana yake siku kabla ya Siku ya Sabato.) Jua lilikuwa bado halijazama. Yusufu wa Arimathea alifika. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Kiyahudi aliyeheshimiwa, ambaye pia alikuwa anautazamia ufalme wa Mungu unaokuja. Kwa ujasiri mkubwa aliingia kwa Pilato na kuuomba mwili wa Yesu. Pilato alishangaa Yesu angekuwa amekufa kwa haraka namna hii, hivyo alimwita yule akida na kumwuliza kama Yesu alikuwa tayari amekufa. Aliposikia taarifa kutoka kwa yule afisa wa jeshi, ndipo alipoutoa mwili wa Yesu na kumpa Yusufu wa Arimathea. Hivyo Yusufu alinunua mavazi kadhaa ya hariri, na akamshusha Yesu toka msalabani, akauzungushia mwili wake na hariri hiyo, na kumweka katika kaburi lililokuwa limechongwa katika mwamba. Kisha alivingirisha jiwe kubwa na kuliweka mlangoni mwa kaburi. Mariamu Magdalena na Maria mama yake Yose aliona pale alipolazwa Yesu. Sabato ilipomalizika, Mariamu Magdalena, Maria mama yake Yakobo, na Salome wakanunua manukato yenye harufu nzuri ili kuyapaka kwenye mwili wa Yesu. Alfajiri na mapema Jumapili, mara tu baada ya jua kuchomoza, walienda kwenye kaburi la Yesu. Nao walikuwa wakiambiana wao kwa wao, ni nani atakayelivingirisha jiwe litoke katika mlango wa kaburi kwa ajili yetu? Kisha wakatazama juu na wakaona kuwa jiwe lile kubwa lilikuwa limevingirishwa tayari litoke mlangoni mwa kaburi la Yesu. Walipoingia kaburini, wakamwona kijana mmoja ameketi upande wa kulia naye alikuwa amevaa vazi jeupe, nao wakastaajabu. Naye akamwambia, “Usistaajabu. Unamtafuta Yesu wa Nazareti, aliyesulubiwa? Tazama amefufuka! Hayupo hapa. Angalieni mahali walipokuwa wameweka mwili wake. Hata hivyo nendeni na kuwaeleza wafuasi wake pamoja na Petro kwamba: ‘Ametangulia mbele yenu kuelekea Galilaya. Mtamkuta kule, kama alivyowaambia.’” Kwa hiyo wale wanawake walitoka na kukimbia kutoka kaburini, kwa sababu hofu na mshangao ulikuwa umewajia. Nao hawakusema chochote kwa mtu yeyote kwani waliogopa. Baada ya Yesu kufufuka alfajiri na mapema siku ya Jumapili, alimtokea kwanza Maria Magdalena, ambaye awali alifukuza mashetani saba kutoka kwake. Baada ya Mariamu kumwona Yesu, alienda na kuwaeleza wanafunzi wake. Walikuwa wamehuzunishwa sana na walikuwa wakilia. Lakini Mariamu aliwaambia kwamba Yesu yu hai. Aliwaambia ya kwamba yeye amemwona, lakini wao hawakumwamini. Baada ya hayo, Yesu kwa namna tofauti akawatokea wanafunzi wake wawili walipokuwa wakitembea kuelekea mashambani. Hawa kisha walirudi na wakawasimulia wengine wote, lakini nao hawakuwaamini. Baadaye, Yesu aliwatokea wale mitume kumi na mmoja walipokuwa wakila. Naye akawakaripia kwa kutokuwa na imani. Walikuwa wakaidi na walikataa kuwaamini wale waliomwona Yesu baada ya kufufuka kwake. Naye akawaambia, “Nendeni ulimwenguni pote, na mkahubiri Habari Njema kwa uumbaji wote. Yeyote atakayeamini na kubatizwa ataokolewa, lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. Na wale waaminio wataweza kufanya ishara hizi kama uthibitisho: watafukuza mashetani kwa jina langu; watasema kwa lugha mpya wasizojifunza bado; watakamata nyoka kwa mikono yao; na ikiwa watakunywa sumu yoyote, haitawadhuru; wataweka mikono yao kwa wagonjwa, nao watapona.” Hivyo baada ya Bwana Yesu kuzungumza nao, alichukuliwa mbinguni, kuketi katika mkono wa kuume wa Mungu. Na mitume wakatoka na kwenda kuhubiri kila mahali, na Bwana alifanya kazi pamoja nao akithibitisha kuwa ujumbe wao ni wa kweli kwa ishara zilizofuatana na mahubiri yao. Mheshimiwa Theofilo: Watu wengine wengi wamejaribu kuandika juu ya mambo yaliyotokea katikati yetu ili kuukamilisha mpango wa Mungu. Mambo hayo waliyoyaandika yanalingana na yale tuliyosikia kutoka kwa watu walioyaona tangu mwanzo. Na walimtumikia Mungu kwa kuwaambia wengine ujumbe wake. Nimechunguza kila kitu kwa makini tangu mwanzo. Na nimeona kuwa ni vyema nikuandikie kwa mpangilio mzuri. Nimefanya hivi ili uwe na uhakika kuwa yale uliyofundishwa ni ya kweli. Herode alipokuwa mfalme wa Uyahudi, alikuwepo kuhani mmoja aliyeitwa Zakaria, aliyekuwa mmoja wa makuhani wa kikundi cha Abiya. Mkewe alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Haruni, na jina lake alikuwa Elizabeti. Wote wawili Zakaria na Elizabeti walikuwa wema waliompendeza Mungu na daima walifanya yote yaliyoamriwa na Bwana na kila mara walifuata maagizo yake kwa ukamilifu. Lakini hawakuwa na watoto kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa, na wote wawili walikuwa wazee sana. Ilipofika zamu ya kundi la Zakaria kuhudumu Hekaluni, yeye mwenyewe alikuwepo ili kuhudumu kama kuhani mbele za Mungu kwa ajili kundi. Makuhani walikuwa wanapiga kura kumchagua mmoja wao atakayeingia katika Hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na Zakaria alichaguliwa wakati huu. Wakati wa kufukiza uvumba ulipofika watu wote walikusanyika nje ya Hekalu wakiomba. Zakaria akiwa ndani ya Hekalu alitokewa na malaika wa Bwana akiwa amesimama mbele yake upande wa kulia wa madhabahu ya uvumba. Zakaria alipomwona malaika aliogopa, na akaingiwa na hofu. Lakini Malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria. Mungu amelisikia ombi lako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. Utafurahi sana, na watu wengine wengi watamfurahia pamoja nawe. Atakuwa mkuu kwa ajili ya Bwana. Kamwe asinywe mvinyo wala kitu chochote kile kitakachomlewesha. Atajazwa Roho Mtakatifu tangu akiwa tumboni mwa mama yake. Naye atawafanya Waisraeli wengi wamrudie Bwana Mungu wao. Atamtangulia Bwana ili kuwaandaa watu kuupokea ujio wake. Atakuwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha wazazi na watoto wao na kuwafanya wale wasiomtii Mungu kubadilika na kuanza kumtii Mungu.” Zakaria akamwambia malaika, “Nitajuaje kuwa haya unayosema ni ya kweli? Maana mimi ni mzee na mke wangu ana umri mkubwa pia.” Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, ambaye daima husimama mbele za Mungu nikiwa tayari. Amenituma kuzungumza nawe na kukujulisha habari hizi njema. Sasa sikiliza! Hautaweza kuzungumza mpaka siku ambayo mambo haya yatatokea kwa sababu hukuyaamini yale niliyokwambia. Lakini nilichosema hakika kitatokea.” Watu waliokuwa nje ya Hekalu wakimngojea Zakaria walishangaa kwa sababu alikaa kwa muda mrefu ndani ya Hekalu. Zakaria alipotoka nje hakuweza kuzungumza nao. Aliwafanyia watu ishara kwa mikono yake. Hivyo watu walitambua kuwa alikuwa ameona maono alipokuwa Hekaluni. Zamu ya utumishi wake ilipokwisha alirudi nyumbani. Wakati fulani baadaye, Elizabeti, mke wa Zakaria akawa mjamzito. Alikaa katika nyumba yake na hakutoka nje kwa miezi mitano. Alisema, “Na sasa, hatimaye Bwana amenisaidia kwa kuniondolea aibu yangu.” Mwezi wa sita wa ujauzito wa Elizabeti, Mungu alimtuma malaika Gabrieli kwa msichana mmoja bikira aliyeishi Nazareti, mji wa Galilaya. Msichana huyo alikuwa amechumbiwa na Yusufu mzaliwa katika ukoo wa Daudi. Jina la bikira huyo lilikuwa Mariamu. *** Malaika alimwendea na kusema “Salamu! Bwana yu pamoja nawe; Kwa kuwa neema yake iko juu yako.” Lakini, Mariamu alichanganyikiwa kutokana na yale aliyosema malaika. Akajiuliza, “Salamu hii ina maana gani?” Malaika akamwambia, “Usiogope Mariamu, kwa kuwa neema ya Mungu iko juu yako. Sikiliza! Utapata mimba na kuzaa mtoto mwanamume, nawe utamwita jina lake Yesu. Mtoto huyo atakuwa Mkuu na watu watamwita Mwana wa Mungu Aliye Mkuu Sana na Bwana Mungu atamfanya kuwa mfalme kama Daudi baba yake. Naye ataitawala nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Mariamu akamwambia malaika, “Jambo hili litatokeaje? Kwa maana mimi bado ni bikira.” Malaika akamwambia Mariamu, “Roho Mtakatifu atakujia, na nguvu zake Mungu Mkuu zitakufunika. Na hivyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu na ataitwa Mwana wa Mungu. Pia sikiliza hili: Jamaa yako Elizabeti ni mjamzito. Ijapokuwa ni mzee sana, atazaa mtoto wa kiume. Kila mtu alidhani hataweza kuzaa, lakini sasa huu ni mwezi wa sita wa ujauzito wake. Mungu anaweza kufanya jambo lolote!” Mariamu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, basi jambo hili litokee kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka. Mariamu akajiandaa na kwenda haraka katika mji mmoja ulio vilimani katika jimbo la Yuda. Alikwenda nyumbani kwa Zakaria, alipofika akamsalimu Elizabeti. Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akirukaruka, na Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu. Kisha akapaza sauti na kumwambia Mariamu, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mtoto utakayemzaa amebarikiwa. Lakini jambo hili kuu limetokeaje kwangu, hata mama wa Bwana wangu aje kwangu? Kwa maana sauti ya salamu yako ilipofika masikioni mwangu, mtoto aliye ndani yangu amerukaruka kwa furaha. Umebarikiwa wewe uliyeamini kuwa mambo aliyokuambia Bwana yatatokea.” Mariamu akasema, “Moyo wangu unamwadhimisha Bwana, kwa maana, Yeye, Mungu na Mwokozi wangu amenipa furaha kuu! Kwa maana ameonesha kunijali, mimi mtumishi wake, nisiye kitu. Na kuanzia sasa watu wote wataniita mbarikiwa. Kwa kuwa Mwenye Nguvu amenitendea mambo makuu. Jina lake ni takatifu. Na huwapa rehema zake wale wamchao, kutoka kizazi hadi kizazi. Ameonesha nguvu ya mkono wake; Amewatawanya wanaojikweza. Amewaangusha watawala kutoka katika viti vyao vya enzi, na kuwakweza wanyenyekevu. Amewashibisha wenye njaa kwa mambo mema, na amewatawanya matajiri bila ya kuwapa kitu. Amemsaidia Israeli, watu aliowachagua ili wamtumikie. Amekumbuka kuonesha rehema; Maana ndivyo alivyowaahidi baba zetu, Ibrahimu na wazaliwa wake.” Mariamu alikaa na Elizabeti kwa muda wa kama miezi mitatu, kisha alirudi nyumbani kwake. Wakati ulipotimia kwa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume. Majirani na jamaa zake waliposikia jinsi Bwana alivyokuwa mwema kwake, walifurahi pamoja naye. Mtoto alipofikisha umri wa siku nane, walikuja kumtahiri. Walipotaka kumwita mtoto Zakaria kutokana na jina la baba yake. Mama yake akasema, “Hapana, mtoto ataitwa Yohana.” Lakini wao wakamwambia, “Hakuna jamaa yako hata mmoja mwenye jina hilo.” Ndipo wakamfanyia ishara baba yake wakimwuliza jina alilotaka kumpa mtoto. Zakaria akataka ubao wa kuandikia, Kisha akaandika, “Jina lake ni Yohana.” Wote wakashangaa. Mara hiyo hiyo mdomo wake ulifunguliwa na ulimi wake ukaachia, akaanza kuzungumza na kumsifu Mungu. Majirani zao wakajawa hofu na watu katika sehemu zote za vilima katika jimbo la Yuda wakawa wanazungumza kuhusu jambo hili. Watu wote waliosikia kuhusu mambo haya walijiuliza, wakisema, “Mtoto huyu atakuwa wa namna gani?” Kwa kuwa nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye. Kisha Zakaria, baba yake Yohana, akajaa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema: “Asifiwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amekuja kuwasaidia watu wake na kuwaweka huru. Na ametuletea sisi Mwokozi Mwenye Nguvu, kutoka katika ukoo wa mtumishi wake Daudi. Hivi ndivyo alivyoahidi kupitia manabii wake watakatifu tangu zamani. Aliahidi kwa Agano kuwa atatuokoa na adui zetu na milki za wote wanaotuchukia. Ili kuonesha rehema kwa baba zetu, na kulikumbuka agano lake takatifu aliloagana nao. Agano hili ni kiapo alichomwapia baba yetu Ibrahimu. Alipoahidi kutuokoa kutoka katika nguvu za adui zetu, ili tuweze kumwabudu Yeye bila hofu. Katika namna iliyo takatifu na yenye haki mbele zake siku zote za maisha yetu. Sasa wewe, mtoto mdogo, utaitwa nabii wa Mungu Aliye Juu Sana, kwa sababu utamtangulia Bwana kuandaa njia yake. Utawaambia watu wake kwamba wataokolewa kwa kusamehewa dhambi zao. Kwa rehema ya upendo wa Mungu wetu, siku mpya itachomoza juu yetu kutoka mbinguni. Kuwaangazia wale wanaoishi katika giza, kwa hofu ya mauti, na kuongoza hatua zetu katika njia ya amani.” Na hivyo mtoto Yohana akakua na kuwa na nguvu katika roho. Kisha akaishi maeneo yasiyo na watu mpaka wakati alipotokea hadharani akihubiri ujumbe wa Mungu kwa watu wa Israeli. Ulikuwa wakati ambapo amri ilitolewa na Kaisari Augusto kwamba watu wote wanaoishi katika utawala wote wa Rumi wahesabiwe na kuorodheshwa katika kumbukumbu za serikali. Orodha hii ilikuwa ya kwanza tangu Kirenio alipokuwa gavana wa Shamu. Kila mtu alikwenda katika mji aliozaliwa ili akahesabiwe na kuingizwa katika orodha hiyo. Hivyo Yusufu alitoka Nazareti, mji uliokuwa katika jimbo la Galilaya na kwenda katika mji wa Bethlehemu uliokuwa katika jimbo la Uyahudi. Pia, mji huu ulijulikana kama mji wa Daudi. Yusufu alikwenda Bethlehemu kwa sababu alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Daudi. Yusufu alijiandikisha akiwa pamoja na Mariamu kwani alikuwa tayari amemchumbia ili amwoe. Na Mariamu alikuwa mjamzito. Yusufu na Mariamu walipokuwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu kujifungua ulifika. Akamzaa mwanawe wa kwanza. Akamvingirishia nguo vizuri, kisha akamlaza katika hori la kulishia mifugo. Walimweka humo kwa sababu chumba cha wageni kilikuwa kimejaa. Usiku ule, baadhi ya wachungaji walikuwa mashambani nje ya mji wa Bethlehemu wakilinda kondoo zao. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukaangaza kuwazunguka, wakaogopa sana. Malaika akawaambia, “Msiogope, kwa kuwa nimewaletea habari njema zitakazowafurahisha watu wa Mungu wote. Kwa sababu leo katika mji wa Daudi amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo, Bwana. Na hivi ndivyo mtakavyomtambua: Mtamkuta mtoto mchanga amevingirishiwa nguo na amelala katika hori la kulishia mifugo.” Kisha malaika pamoja na jeshi kubwa la mbinguni wakaanza kumsifu Mungu, wakisema: “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na amani iwepo duniani kwa watu wote wanaompendeza.” Malaika walipoondoka kurudi mbinguni, wale wachungaji wakaambiana wakisema, “Twendeni Bethlehemu, tukalione jambo hili lililotokea, ambalo Bwana ametujulisha.” Wakaenda haraka, wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala katika hori la kulishia mifugo. Wachungaji walipomwona huyo mtoto, walisimulia kile walichoambiwa na malaika kuhusu mtoto. Kila aliyesikia maelezo ya wachungaji, alishangaa. Mariamu aliendelea kuyatafakari mambo haya, na kuyaweka moyoni. Wachungaji waliirudia mifugo yao, wakawa wanamsifu na kumshukuru Mungu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona. Ilikuwa kama walivyoambiwa na malaika. Ilipofika siku ya nane mtoto alitahiriwa, akaitwa Yesu. Hili ndilo jina alilopewa na malaika kabla mama yake hajaibeba mimba yake. Muda wa kutakaswa ulimalizika, kama ilivyotakiwa na Sheria ya Musa baada ya mtoto kuzaliwa. Baada ya hapo walimpeleka Yesu Yerusalemu na kumweka mbele za Bwana. Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana: Mzaliwa wa kwanza akiwa mtoto wa kiume, atolewe wakfu kwa ajili ya Bwana. Pia Mariamu na Yusufu walikwenda Yerusalemu kutoa dhabihu kama Sheria ya Bwana inavyosema kuwa, “Ni lazima utoe dhabihu ya jozi moja ya hua au makinda mawili wa njiwa.” Alikuwepo mtu mmoja aliyeishi katika mji wa Yerusalemu, mtu huyu aliitwa Simeoni. Alikuwa mtu mwema na mcha Mungu na Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. Alikuwa akiusubiri wakati ambao Mungu angeisaidia Israeli. Roho Mtakatifu alimwambia kwamba asingekufa kabla ya kumwona Masihi kutoka kwa Bwana. Roho Mtakatifu alimwongoza mpaka Hekaluni. Hivyo, alikuwemo Hekaluni wakati Mariamu na Yusufu walipomleta mtoto Yesu ili wamfanyie kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Kiyahudi. Simeoni alimbeba mtoto Yesu mikononi mwake, akamshukuru Mungu na kusema, “Sasa, Bwana, niruhusu mimi mtumishi wako nife kwa amani kwa kuwa umeitimiza ahadi yako kwangu. Nimeona kwa macho yangu namna utakavyowaokoa watu wako. Sasa watu wote wanaweza kuuona mpango wako. Yeye ni mwanga wa kuionesha njia yako kwa mataifa mengine, na atawaletea heshima watu wako Israeli.” Mariamu na Yusufu walishangazwa sana na maneno aliyosema Simeoni kuhusu Yesu. Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu; “Wayahudi wengi wataanguka na wengi watainuka kwa sababu ya mtoto huyu. Atakuwa ishara kutoka kwa Mungu, lakini baadhi ya watu watamkataa. Mawazo ya siri ya watu wengi yatajulikana. Na mambo yatakayotokea yatakuumiza, kama upanga unaokuchoma moyoni.” Alikuwapo nabii aliyeitwa Ana binti Fanueli, kutoka katika kabila la Asheri. Alikuwa mwanamke mzee sana. Aliishi na mume wake kwa miaka saba, kabla ya mume wake kufa na kumwacha peke yake. Na sasa alikuwa na umri wa miaka themanini na nne. Ana alikuwa Hekaluni daima, hakutoka. Alimwabudu Mungu kwa kufunga na kuomba usiku na mchana. Simeoni alipokuwa anazungumza na Yusufu na Mariamu, Ana alikwenda walipokuwa na akaanza kumsifu Mungu na kuwaambia kuhusu Yesu watu wote waliokuwa wanasubiri Mungu kuikomboa Yerusalemu. Yusufu na Mariamu walipotimiza mambo yote yanayotakiwa katika sheria ya Bwana, walirudi Galilaya, katika mji wao wa Nazareti. Mtoto Yesu aliendelea kukua na kuwa kijana mwenye nguvu na aliyejaa hekima nyingi. Na Mungu alikuwa anambariki. Kila mwaka wazazi wa Yesu walikwenda Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, walikwenda kwenye sikukuu kama ilivyokuwa desturi ya Kiyahudi. Sikukuu ilipokwisha, walirudi nyumbani, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kutambua. Walianza kumtafuta kwa jamaa na rafiki zao baada ya kusafiri kutwa nzima, wakidhani kuwa alikuwa pamoja nao katika msafara. Walipomkosa, walirudi Yerusalemu kumtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamkuta Hekaluni, amekaa katikati ya walimu wa dini, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Na wote waliomsikiliza walishangazwa sana kwa ufahamu wake na majibu yake ya busara. Wazazi wake walipomwona walishangaa pia, ndipo mama yake akamwambia, “Mwanangu, kwa nini umefanya hivi? Mimi na baba yako tulikuwa na wasiwasi sana, na tumekuwa tukikutafuta.” Yesu akawaambia, “Kwa nini mlikuwa mnanitafuta? Mnapaswa kujua kuwa inanilazimu kuwemo nyumbani mwa Baba yangu?” Lakini wao hawakuelewa alichowaambia. Yesu alirudi pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii. Mama yake aliendelea kuyaweka mambo haya yote moyoni mwake. Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu. Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, ambapo: Pontio Pilato alikuwa gavana wa Uyahudi; Herode alikuwa mtawala wa Galilaya; Filipo ndugu yake Herode alikuwa mtawala wa Iturea na Trakoniti; na Lisania, alikuwa mtawala wa Abilene. Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Katika kipindi hiki, Yohana, mwana wa Zakaria, alikuwa akiishi jangwani na alipata ujumbe kutoka kwa Mungu. Alipita katika maeneo yote yaliyo karibu na Mto Yordani akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. Hii ni kama maneno yaliyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya, yanayosema, “Kuna mtu anayeipaza sauti yake kutokea nyikani: ‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana; nyoosheni njia kwa ajili yake. Kila bonde litajazwa, na kila mlima na kilima vitasawazishwa. Barabara zilizopinda zitanyooshwa, na barabara zenye mashimo zitasawazishwa. Na kila mtu ataona jinsi Mungu atakavyowaokoa watu wake.’” Makundi ya watu walimwendea Yohana ili awabatize. Lakini aliwaambia, “Enyi nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja? Badilisheni mioyo yenu! Kisha onesheni ya kuwa mmebadilika kwa namna mnavyoishi. Ninajua mtasema kuwa, ‘Ibrahimu ni baba yetu.’ Hilo halijalishi chochote. Ninawaambia Mungu anaweza kumwumbia Ibrahimu watoto kutokana na mawe haya! Na sasa shoka liko tayari kukata miti, kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.” Watu wakamwuliza Yohana, “Tufanye nini?” Akajibu, “Ukiwa na mashati mawili mpe moja asiyekuwa na shati. Kama una chakula, kigawe pia.” Hata watoza ushuru walikuja kwa Yohana. Walitaka wabatizwe. Walimwambia, “Mwalimu, tufanye nini sisi?” Akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi kuliko kiwango kilichoamriwa.” Askari wakamwuliza, “Vipi kuhusu sisi? Tufanye nini?” Akawaambia, “Msitumie nguvu au kutengeneza mashtaka ya uongo ili watu wawape pesa. Mtosheke na mishahara mnayopata.” Kila mtu alitarajia kuja kwa Masihi, na walijiuliza wakisema, “Labda Yohana ndiye Masihi.” Yohana aliwajibu watu wote, akasema, “Ninawabatiza ninyi katika maji, lakini yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, huyo atafanya mengi zaidi yangu. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Yeye huyo atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Yuko tayari sasa kuja kusafisha nafaka. Atatenganisha nafaka nzuri na makapi, na kuiweka katika ghala yake kisha ataichoma ile isiyofaa katika moto usiozimika.” Hivi ndivyo ambavyo Yohana aliwahubiri watu Habari Njema. Aliwaonya sana kuwa wanatakiwa kubadili njia zao. Yohana alimkosoa Herode kwa sababu ya mambo mabaya aliyokuwa ameyafanya na Herodia, mkewe kaka yake Herode, na pia kwa mambo mengine mabaya aliyokuwa ameyafanya. Hivyo Herode aliongeza jambo jingine baya katika matendo yake maovu. Alimfunga Yohana gerezani. Watu wote walipokuwa wakibatizwa, Yesu alikuja naye akabatizwa. Na alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka, na Roho Mtakatifu aliyekuwa katika umbo la njiwa akashuka juu yake. Sauti ikasikika toka mbinguni, “Wewe ni mwanangu, ninayekupenda, napendezwa nawe sana.” Yesu alipoanza kufundisha, alikuwa na umri kama wa miaka thelathini. Watu walidhani kuwa Yesu alikuwa Mwana wa Yusufu. Yusufu alikuwa mwana wa Eli. Eli alikuwa mwana wa Mathati. Mathati alikuwa mwana wa Lawi. Lawi alikuwa mwana wa Melki. Melki alikuwa mwana wa Yana. Yana alikuwa mwana wa Yusufu. Yusufu alikuwa mwana wa Matathia. Matathia alikuwa mwana wa Amosi. Amosi alikuwa mwana wa Nahumu. Nahumu alikuwa mwana wa Esli. Esli alikuwa mwana wa Nagai. Nagai alikuwa mwana wa Maathi. Maathi alikuwa mwana wa Matathia. Matathia alikuwa mwana wa Semei. Semei alikuwa mwana wa Yusufu. Yusufu alikuwa mwana wa Yoda. Yoda alikuwa mwana wa Yoana. Yoana alikuwa mwana wa Resa. Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli. Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli. Shealtieli alikuwa mwana wa Neri. Neri alikuwa mwana wa Melki. Melki alikuwa mwana wa Adi. Adi alikuwa mwana wa Kosamu. Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu, Elmadamu alikuwa mwana wa Eri. Eri alikuwa mwana wa Yoshua. Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri. Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu. Yorimu alikuwa mwana wa Mathati. Mathati alikuwa mwana wa Lawi. Lawi alikuwa mwana wa Simeoni. Simeoni alikuwa mwana wa Yuda. Yuda alikuwa mwana wa Yusufu. Yusufu alikuwa mwana wa Yonamu. Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu. Eliakimu alikuwa mwana wa Melea. Melea alikuwa mwana wa Mena. Mena alikuwa mwana wa Matatha. Matatha alikuwa mwana wa Nathani. Nathani alikuwa mwana wa Daudi. Daudi alikuwa mwana wa Yese. Yese alikuwa mwana wa Obedi. Obedi alikuwa mwana wa Boazi. Boazi alikuwa mwana wa Salmoni. Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni. Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu. Aminadabu alikuwa mwana wa Admini, Admini alikuwa mwana wa Aramu. Aramu alikuwa mwana wa Hesroni. Hesroni alikuwa mwana wa Peresi. Peresi alikuwa mwana wa Yuda. Yuda alikuwa mwana wa Yakobo. Yakobo alikuwa mwana wa Isaka. Isaka alikuwa mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alikuwa mwana wa Tera. Tera alikuwa mwana wa Nahori. Nahori alikuwa mwana wa Serugi, Serugi alikuwa mwana wa Ragau. Ragau alikuwa mwana wa Pelegi. Pelegi alikuwa mwana wa Eberi, Eberi alikuwa mwana wa Sala. Sala alikuwa mwana wa Kenani. Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi. Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu. Shemu alikuwa mwana wa Nuhu. Nuhu alikuwa mwana wa Lameki. Lameki alikuwa mwana wa Methusela. Methusela alikuwa mwana wa Henoko. Henoko alikuwa mwana wa Yaredi. Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli. Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani. Kenani alikuwa mwana wa Enoshi. Enoshi alikuwa mwana wa Sethi. Sethi alikuwa mwana wa Adamu. Adamu alikuwa mwana wa Mungu. Akiwa amejaa Roho Mtakatifu, Yesu akarudi kutoka Mto Yordani. Kisha Roho Mtakatifu akamwongoza mpaka nyikani kwa muda wa siku arobaini, alikojaribiwa na Ibilisi. Katika muda wote huo hakula chakula chochote na baadaye akahisi njaa sana. Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate.” Yesu akamjibu, “Maandiko yanasema, ‘Watu hawataishi kwa mkate tu.’” Kisha mwovu akamchukua Yesu na kwa muda mfupi akamwonyesha falme zote za ulimwengu. Mwovu akamwambia, “Nitakufanya uwe mfalme wa sehemu zote hizi. Utakuwa na mamlaka juu yao, na utapata utukufu wote. Yote yametolewa kwangu. Ninaweza kumpa yeyote kadri ninavyopenda. Nitakupa vyote hivi, ikiwa utaniabudu tu.” Yesu akajibu, “Maandiko yanasema, ‘Ni lazima umwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’” Ndipo Shetani akamwongoza Yesu mpaka Yerusalemu na kumweka mahali palipo juu katika mnara wa Hekalu. Akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe! Kwani Maandiko yanasema, ‘Mungu atawaamuru malaika zake wakulinde.’ Pia imeandikwa kuwa, ‘Mikono yao itakudaka, ili usijikwae mguu wako kwenye mwamba.’” Yesu akajibu, “Pia, Maandiko yanasema: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’” Shetani alipomaliza kumjaribu Yesu katika namna zote, alimwacha akaenda zake hadi wakati mwingine. Yesu alirudi Galilaya akiwa na nguvu za Roho Mtakatifu. Habari zake zilisambaa katika eneo lote lililozunguka Galilaya. Alianza kufundisha katika masinagogi na kila mtu alimsifu. Yesu alisafiri akaenda katika mji aliokulia wa Nazareti. Siku ya Sabato alikwenda kwenye sinagogi kama alivyokuwa akifanya. Alisimama ili asome. Akapewa gombo la nabii Isaya. Akalivingirisha kulifungua na akapata mahali palipoandikwa haya: “Roho wa Bwana yu juu yangu, amenichagua ili niwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na kuwaambia wasiyeona kuwa wanaweza kuona tena. Amenituma kuwapa uhuru wale wanaoteswa na kutangaza kuwa wakati wa Bwana kuonesha wema wake umefika.” Yesu akalivingirisha gombo akalifunga, akalirudisha kwa msaidizi na kuketi chini. Kwa kuwa kila mtu ndani ya sinagogi alimwangalia kwa makini, Alianza kuzungumza nao. Akasema, “Maandiko haya yametimilika mlipokuwa mnanisikia nikiyasoma!” Kila mtu pale akasema alipenda namna ambavyo Yesu alizungumza. Walishangaa kumsikia akisema maneno haya ya ajabu. Wakaulizana, “Inawezekanaje? Huyu si mwana wa Yusufu?” Yesu akawaambia, “Ninafahamu mtaniambia mithali hii ya zamani: ‘Daktari, jitibu mwenyewe.’ Mnataka kusema ‘Tulisikia mambo yote uliyotenda Kapernaumu. Yatende pia hapa katika mji wako mwenyewe!’” Lakini Yesu akasema, “Ukweli ni huu, nabii hakubaliki katika mji wa kwao. Wakati wa Eliya mvua haikunyesha katika Israeli kwa miaka mitatu na nusu. Chakula hakikuwepo mahali popote katika nchi yote. Palikuwa wajane wengi katika Israeli wakati huo. Lakini Eliya hakutumwa kwenda kwa mmoja wa wajane waliokuwa katika Israeli bali kwa mjane aliyekuwa katika mji wa Sarepta, jirani na Sidoni. *** Na, palikuwa wenye ugonjwa mbaya wa ngozi wengi walioishi katika Israeli wakati wa nabii Elisha, lakini hakuna aliyeponywa isipokuwa Naamani, aliyetoka katika nchi ya Shamu, siyo Israeli.” Watu wote waliposikia hili, walikasirika sana. Wakasimama na kumlazimisha Yesu atoke nje ya mji. Mji wao ulijengwa juu ya kilima. Wakamchukua Yesu mpaka ukingo wa kilima ili wamtupe. Lakini alipita katikati yao na kwenda zake. Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji uliokuwa Galilaya. Siku ya Sabato aliwafundisha watu. Nao walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha kwa sababu mafundisho yake yalikuwa na mamlaka. Ndani ya sinagogi alikuwepo mtu aliyekuwa na roho chafu, kutoka kwa yule Mwovu, ndani yake. Akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, “Aiii! Unataka nini kwetu Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani; Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.” Lakini Yesu akamkemea yule pepo na kumwambia, “Nyamaza kimya! Umtoke mtu huyu!” Ndipo pepo akamtupa yule mtu chini mbele ya watu, akamtoka bila kumjeruhi sehemu yoyote ya mwili wake. Watu wakashangaa. Wakasemezana wao kwa wao, “Hii inamaanisha nini? Kwa mamlaka na uwezo anaamuru pepo wachafu na wanatoka!” Hivyo habari kuhusu Yesu zikaenea kila mahali katika eneo lote. Yesu akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mkwe wa Simoni alikuwa mgonjwa sana. Alikuwa na homa kali. Nao walimwomba Yesu amsaidie. Yesu alisimama karibu yake na kuiamuru homa kuondoka. Homa ikamwacha, naye akasimama na kuanza kuwahudumia. Jua lilipokuchwa, watu wote waliwaleta kwa Yesu jamaa na rafiki zao walioumwa na wenye magonjwa mengi tofauti. Yesu aliweka mikono yake juu ya kila mgonjwa na kuwaponya wote. Pepo nao waliwatoka watu wengi. Mapepo yalipiga kelele yakisema “Wewe ni Mwana wa Mungu.” Lakini Yesu alitoa amri yenye nguvu kwa mapepo yasiseme, kwa sababu yalijua alikuwa ni Masihi. Siku iliyofuata Yesu alijitenga na kwenda mahali ili awe peke yake. Watu wakawa wakimtafuta. Walipompata, walijaribu kumzuia asiondoke. Lakini akawaambia, “Ni lazima nihubiri Habari Njema kuhusu Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa sababu nilitumwa kufanya hivyo.” Kisha Yesu akahubiri Habari Njema katika masinagogi ya Uyahudi. Yesu aliposimama ukingoni mwa Ziwa Galilaya kundi la watu lilimsogelea ili wasikie mafundisho kuhusu Mungu. Yesu aliona mashua mbili zikiwa kando ya ziwa. Wavuvi walikuwa wametoka katika mashua zao na walikuwa wanaosha nyavu zao. Yesu aliingia kwenye mashua ya Simoni. Akamwomba Simoni aisogeze mbali kidogo na ufukwe wa ziwa. Kisha akaketi ndani ya mashua na akawafundisha watu waliokuwa ufukweni mwa ziwa. Yesu alipomaliza kufundisha, alimwambia Simoni, “Ipeleke mashua mpaka kwenye kilindi cha maji kisha mshushe nyavu zenu majini na mtapata samaki.” Simoni akamjibu, “Bwana, tumejitahidi usiku kucha kuvua samaki na hatukupata chochote. Lakini kwa kuwa unasema nishushe nyavu majini, nitafanya hivyo.” Walipofanya hivi, nyavu zao zilijaa samaki wengi mpaka zikaanza kuchanika. Waliwaita rafiki zao waliokuwa katika mashua nyingine ili waje wawasaidie. Rafiki zao walikuja kuwasaidia, na mashua zote mbili zilijaa samaki kiasi cha kutaka kuzama. Wavuvi wote walistaajabu kwa sababu ya wingi wa samaki waliovua. Simoni Petro alipoona hili, akapiga magoti mbele ya Yesu na akasema, “Nenda mbali nami Bwana, mimi ni mwenye dhambi!” *** Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo, walishangaa pia. (Yakobo na Yohana walikuwa wanavua pamoja na Simoni.) Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope. Kuanzia sasa kazi yako haitakuwa kuvua samaki bali kukusanya watu!” Wakaziendesha mashua zao mpaka pwani, kisha wakaacha kila kitu na kumfuata Yesu. Wakati mmoja Yesu alikuwa katika mji ambao mwanaume mmoja mgonjwa alikuwa anaishi. Mwanaume huyo alikuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi mwili wake wote. Alipomwona Yesu, alimsujudia na kumsihi akisema, “Bwana, ikiwa unataka una uwezo wa kuniponya.” Yesu akasema, “Hakika ninataka kukuponya, upone!” Kisha akamgusa, na ugonjwa ukatoweka papo hapo. Yesu akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze. Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona.” Lakini habari kuhusu Yesu zilizidi kuenea zaidi. Watu wengi walikuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Mara nyingi Yesu alikwenda sehemu zingine zisizokuwa na watu na akaomba huko. Siku moja Yesu alikuwa anawafundisha watu. Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wameketi hapo pia. Walitoka katika kila mji wa Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu. BWANA alimpa Yesu uwezo wa kuponya watu. Alikuwepo mtu aliyepooza na baadhi ya watu walikuwa wamembeba kwenye machela. Walijaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu. Lakini walishindwa kufika alipokuwa Yesu kwa sababu kulikuwa na watu wengi sana. Hivyo walikwenda juu ya paa ya nyumba na kumshusha aliyepooza chini kupitia tundu kwenye dari. Waliishusha machela alimokuwa aliyepooza kwa usawa kiasi kwamba akawa amelala mbele ya Yesu. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo, akamwambia yule mgonjwa: “Rafiki yangu, dhambi zako zimesamehewa!” Walimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wao kwa wao wakisema: “Huyu mtu ni nani kiasi cha kuthubutu kusema hivi? Si anamtukana Mungu! Mungu peke yake ndiye anayesamehe dhambi.” Lakini Yesu alijua walichokuwa wanawaza, akawaambia: “Kwa nini mna maswali haya mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa.’ Kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia, mtu huyu, beba machela yako na utembee? Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina.” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, Inuka! Beba machela yako uende nyumbani!” *** Yule mtu akasimama saa ile ile mbele ya kila mtu. Akaubeba machela yake na kwenda nyumbani kwake, akimsifu Mungu. Kila mtu alishangaa na kuanza kumsifu Mungu. Wakajawa na hofu kuu baada ya kuiona nguvu ya Mungu. Wakasema, “Leo tumeona mambo ya kushangaza!” Baada ya hayo Yesu alitoka nje akamwona mtoza ushuru amekaa sehemu yake ya kukusanyia ushuru. Jina lake aliitwa Lawi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Lawi akasimama, akaacha kila kitu na kumfuata Yesu. Lawi akaandaa chakula cha usiku nyumbani kwake kwa kumheshimu Yesu. Mezani walikuwepo watoza ushuru wengi na baadhi ya watu wengine. Lakini Mafarisayo na wale wanaofundisha sheria kwa ajili ya Mafarisayo wakaanza kulalamika kwa wafuasi wa Yesu wakisema, “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?” Yesu akawajibu, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari, si wenye afya njema. Sikuja kuwaambia wenye haki wabadilike, bali wenye dhambi.” Baadhi ya watu wakamwambia Yesu, “Wafuasi wa Yohana hufunga na kuomba mara kwa mara, vivyo hivyo wafuasi wa Mafarisayo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa kila wakati.” Yesu akawaambia, “Kwenye harusi huwezi kuwaambia marafiki wa bwana harusi wafunge wakati bwana harusi bado yuko pamoja nao. Lakini muda ukifika na bwana harusi akaondolewa kwao. Watakuwa na huzuni, na watafunga.” Yesu akawaambia mfano huu: “Hakuna anayekata kiraka kwenye vazi jipya na kukishona kwenye vazi la zamani. Ataharibu vazi jipya, na kiraka kutoka vazi jipya hakitakuwa sawa na vazi la zamani. Pia hakuna mtu anayeweka divai mpya katika viriba vya zamani. Divai mpya itavipasua, divai itamwagika, na viriba vitaharibika. Daima mnaweka divai mpya kwenye viriba vipya. Hakuna mtu ambaye baada ya kunywa divai ya zamani hutaka divai mpya. Kwa sababu husema, ‘Divai ya zamani ni nzuri.’” Wakati fulani siku ya Sabato, Yesu alikuwa akitembea kupitia katika baadhi ya mashamba ya nafaka. Wafuasi wake wakachukua masuke, wakayapukusa mikononi mwao na kula nafaka. Baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, “Kwa nini mnafanya hivyo? Ni kinyume na Sheria ya Musa kufanya hivyo siku ya Sabato.” Yesu akawajibu, “Je, mmesoma kuhusu jambo alilofanya Daudi, wakati yeye na watu wake walipohisi njaa? Daudi alikwenda katika nyumba ya Mungu, akachukua mikate iliyotolewa kwa Mungu na kuila. Na kuwapa wenzake baadhi ya mikate hiyo. Hii ilikuwa kinyume na Sheria ya Musa, inayosema kuwa makuhani pekee ndiyo wanaoruhusiwa kula mikate hiyo.” Kisha Yesu akawaambia Mafarisayo, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.” Siku nyingine ya Sabato Yesu aliingia katika sinagogi na kuwafundisha watu. Katika sinagogi hili alikuwemo mtu aliyepooza mkono wake wa kulia. Walimu wa sheria na Mafarisayo walikuwa wakimvizia Yesu. Walikuwa wanasubiri waone ikiwa ataponya siku hiyo ya Sabato. Walitaka kumwona akifanya jambo lolote lililo kinyume ili wamshitaki. Lakini Yesu alijua walilokuwa wanawaza. Akamwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyenyuka na simama hapa ambapo kila mtu anaweza kukuona!” Yule mtu akanyenyuka na kusimama pale. Ndipo Yesu akawaambia, “Ninawauliza ninyi, Sheria inaturuhusu tufanye nini siku ya Sabato: kutenda mema au kutenda mabaya? Je, ni halali kuokoa uhai au kuuangamiza?” Yesu akawatazama watu wote kila upande, kisha akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyosha mkono wake, na akaponywa. Mafarisayo na walimu wa sheria wakakasirika sana kiasi cha kutofikiri sawasawa, wakashauriana wao kwa wao wamfanye nini Yesu. Siku chache baadaye, Yesu alikwenda mlimani kuomba. Alikaa huko usiku kucha akimwomba Mungu. Asubuhi iliyofuata aliwaita wafuasi wake, akachagua kumi na wawili miongoni mwao na kuwaita Mitume. Nao ni: Simoni (ambaye Yesu alimwita Petro), Andrea aliyekuwa kaka yake Petro, Yakobo, Yohana, Filipo, Bartholomayo, Mathayo na Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni aliyeitwa Mzelote, Yuda mwana wa Yakobo, na Yuda Iskariote (yule ambaye baadaye alimsaliti Yesu). Yesu na mitume wakatelemka kutoka mlimani. Yesu akasimama mahali tambarare. Kundi kubwa la wafuasi wake lilikuwa pale. Walikuwepo pia watu wengi waliotoka sehemu zote za Uyahudi, Yerusalemu, na maeneo ya pwani karibu na Tiro na Sidoni. Wote walikuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Aliwaponya watu waliokuwa wanasumbuliwa na mapepo. Kila mtu alijaribu kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa unamtoka. Yesu aliwaponya wote. Yesu akawatazama wafuasi wake na kusema, “Heri ninyi mlio maskini. Maana Ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa. Maana mtashibishwa. Heri ninyi mnaolia sasa. Maana mtafurahi na kucheka. Watu watawachukia kwa sababu ninyi ni wa milki ya Mwana wa Adamu. Watawabagua na watawatukana. Watajisikia vibaya hata kutamka majina yenu. Mambo haya yatakapotukia, mjue kuwa baraka kuu ni zenu. Ndipo mfurahi na kurukaruka kwa furaha, kwa sababu mna thawabu kuu mbinguni. Baba zao waliwafanyia manabii vivyo hivyo. Lakini ole wenu ninyi matajiri, kwa kuwa mmekwishapata maisha yenye raha. Ole wenu ninyi mlioshiba sasa, kwa kuwa mtasikia njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtalia na kuhuzunika. Ole wenu watu wote wanapowasifu ninyi. Maana mababu zao waliwasifu manabii wa uongo vivyo hivyo daima. Lakini ninawaambia ninyi mnaonisikiliza, wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wale wanaowachukia. Mwombeni Mungu awabariki wale wanaowalaani ninyi, waombeeni wale wanaowaonea. Mtu akikupiga shavu moja, mwache akupige na la pili pia. Mtu akichukua koti lako, usimkataze kuchukua shati pia. Mpe kila akuombaye kitu. Mtu yeyote akichukua kitu chako, usitake akurudishie. Watendeeni wengine kama mnavyotaka wao wawatendee ninyi. Je, msifiwe kwa sababu ya kuwapenda wale wanaowapenda ninyi tu? Hapana, hata wenye dhambi, wanawapenda wale wanaowapenda. Je, msifiwe kwa kuwa mnawatendea mema wale wanaowatendea mema ninyi? Hapana, hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo! Je, msifiwe kwa kuwa mnawakopesha watu kwa kutarajia kupata vitu kutoka kwao? Hapana, hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wengine, ili warudishiwe kiasi kile kile! Ninawaambia kuwa wapendeni adui zenu na kuwatendea mema. Wakopesheni watu bila kutarajia kitu kutoka kwao. Mkifanya hivyo, mtapata thawabu kuu. Mtakuwa wana wa Mungu Mkuu Aliye Juu. Ndiyo kwa sababu Mungu ni mwema hata kwa wenye dhambi na wasiomshukuru. Iweni na upendo na huruma, kama Baba yenu alivyo. Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa na Mungu. Msiwalaani wengine nanyi hamtalaaniwa. Wasameheni wengine nanyi mtasamehewa. Wapeni wengine vitu, nanyi mtapokea. Mtapewa vingi; kipimo chenye ujazo wa kusukwasukwa na kumwagika. Mungu atawapa ninyi kwa kadri mnavyotoa.” Yesu akawaambia mfano huu, “Je, asiyeona anaweza kumwongoza asiyeona mwenzake? Hapana. Wote wawili watatumbukia shimoni. Wanafunzi si bora kuliko mwalimu wao. Lakini wakiisha kufundishwa na kuhitimu, wanakuwa kama mwalimu wao. Kwa nini unaona kipande kidogo cha vumbi kilicho katika jicho la rafiki yako, lakini hujali kipande cha ubao kilicho ndani ya jicho lako mwenyewe? Unawezaje kumwambia rafiki yako, ‘Hebu nikitoe kipande cha vumbi kilicho katika jicho lako’? Je, huwezi kukiona kipande cha ubao kilicho katika jicho lako mwenyewe? Wewe ni mnafiki. Kwanza kitoe kipande cha ubao katika jicho lako, ndipo utaona vyema na utaweza kukitoa kipande cha vumbi kilicho katika jicho la rafiki yako. Mti mzuri hauzai matunda mabaya. Na mti mbaya hauzai matunda mazuri. Kila mti unatambuliwa kutokana na aina ya matunda unayozaa. Huwezi kupata tini kwenye vichaka vya miiba. Na huwezi kuchuma zabibu kwenye michongoma! Watu wema wana mambo mazuri katika mioyo yao. Ndiyo sababu hutamka mambo mema. Lakini waovu wana mioyo iliyojaa uovu, na ndiyo sababu hutamka mambo maovu. Mambo wanayotamka watu katika midomo yao, ndiyo yaliyojaa katika mioyo yao. Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana’ lakini hamtendi kama ninavyosema? Nitawaonesha namna walivyo watu wanaokuja kwangu, wale wanaoyasikia na kuyatii mafundisho yangu. Ni kama mtu anayejenga nyumba, huchimba chini sana, na kujenga nyumba yake kwenye mwamba. Mafuriko yanapokuja, huigonga nyumba kwa nguvu, nyumba hiyo haiwezi kuanguka kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini watu wanaoyasikia maneno yangu na hawayatii ni kama mtu anayejenga nyumba bila kutayarisha msingi. Mafuriko yanapokuja, nyumba huanguka chini kwa urahisi na kubomoka kabisa.” Yesu alipomaliza kuwaambia watu mambo yote aliyotaka kuwaambia, alikwenda mjini Kapernaumu. Afisa wa jeshi katika mji wa Kapernaumu alikuwa na mtumishi aliyekuwa wa muhimu sana kwake. Mtumishi huyu alikuwa mgonjwa sana karibu ya kufa. Afisa huyu aliposikia kuhusu Yesu, aliwatuma baadhi ya viongozi wa wazee wa Kiyahudi kwa Yesu. Aliwataka wamwombe Yesu aende kumponya mtumishi wake. Wazee walikwenda kwa Yesu, wakamsihi amsaidie afisa. Walisema, “Mtu huyu anastahili msaada wako, Kwa sababu anawapenda watu wetu na ametujengea sinagogi.” Hivyo Yesu alikwenda nao. Alipoikaribia nyumba ya yule afisa, afisa aliwatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, huhitaji kufanya kitu chochote maalumu kwa ajili yangu. Sistahili wewe uingie nyumbani mwangu. Ndiyo maana sikuja mimi mwenyewe kwako. Unahitaji kutoa amri tu na mtumishi wangu atapona. Ninajua hii, kwa kuwa ninaelewa mamlaka. Kuna watu wenye mamlaka juu yangu, na nina askari walio chini ya mamlaka yangu. Nikimwambia askari mmoja ‘nenda’, huenda. Na nikimwambia mwingine ‘njoo’, huja. Pia nikimwambia mtumwa wangu ‘fanya hiki’, hunitii.” Yesu aliposikia hayo alishangaa, akawageukia watu waliokuwa wanamfuata, akawaambia, “Ninawaambia, Sijawahi kuona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.” Kundi lililotumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani, walimkuta yule mtumishi amepona. Siku iliyofuata Yesu na wafuasi wake walikwenda katika mji wa Naini. Kundi kubwa la watu walisafiri pamoja nao. Yesu alipolikaribia lango la mji, aliona watu wamebeba maiti. Alikuwa ni mwana pekee wa mama mjane. Watu wengi kutoka mjini walifuatana na yule mama mjane. Bwana alipomwona yule mama, alimwonea huruma na kumwambia, “Usilie.” Akakaribia, akaligusa jeneza. Wanaume waliokuwa wamebeba jeneza wakasimama. Ndipo Yesu akamwambia kijana aliyekufa, “Kijana, nakuambia, inuka!” Yule kijana, akaketi, akaanza kuongea. Yesu akamrudisha kwa mama yake. Kila mtu aliingiwa hofu. Wakaanza kumsifu Mungu na kusema, “Nabii mkuu yuko hapa pamoja nasi!” na “Mungu amekuja kuwasaidia watu wake!” Habari hii kuhusu Yesu ikaenea katika Uyahudi yote, na kila sehemu kuzunguka pale. Wafuasi wa Yohana Mbatizaji walimweleza Yohana Mbatizaji kuhusu mambo haya yote. Naye aliwaita wanafunzi wake wawili. Akawatuma waende na kumwuliza Yesu, “Wewe ndiye tuliyesikia anakuja, au tumsubiri mwingine?” Wafuasi wa Yohana walipofika kwa Yesu, wakasema, “Yohana Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: ‘Wewe ndiye yule ajaye, au tumsubiri mwingine?’” Wakati ule ule Yesu alikuwa amewaponya watu wengi madhaifu na magonjwa yao. Aliwaponya waliokuwa na pepo wabaya na kuwafanya wasiyeona wengi kuona. Kisha aliwaambia wanafunzi wa Yohana, “Nendeni mkamweleze Yohana yale mliyoyaona na kuyasikia: wasiyeona wanaona, walemavu wa miguu wanatembea, wenye magonjwa mabaya ya ngozi wanatakasika, wasiyesikia wanasikia. Waliokufa wanafufuliwa na Habari Njema inahubiriwa kwa maskini. Heri wale wasio na mashaka kunikubali mimi.” Baada ya wanafunzi wa Yohana kuondoka, Yesu akaanza kuwaambia watu kuhusu Yohana, “Mlitoka kwenda jangwani kuona nini? Mtu aliyekuwa dhaifu, kama unyasi unaotikiswa na upepo? Mlitegemea kuona nini? Mtu aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hilo. Watu wanaovaa mavazi mazuri na kuishi kwa anasa wako katika majumba ya wafalme. Sasa, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yohana ni zaidi ya nabii. Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana: ‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako. Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’ Ninawaambia, hakuna aliyewahi kuzaliwa aliye mkuu kuliko Yohana. Lakini mwenye umuhimu mdogo, katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana.” (Watu waliposikia hili, wote walikubali kuwa mafundisho ya Mungu yalikuwa mazuri. Hata watoza ushuru waliobatizwa na Yohana walikiri. Lakini Mafarisayo na wanasheria walikataa kuukubali mpango wa Mungu kwa ajili yao; hawakumruhusu Yohana awabatize.) “Niseme nini kuhusu watu wa wakati huu? Niwafananishe na nini? Wanafanana na nini? Ni kama watoto waliokaa sokoni. Kundi moja la watoto likawaita watoto wengine na kusema, ‘Tuliwapigia filimbi lakini hamkucheza. Tuliwaimba wimbo wa huzuni, lakini hamkulia.’ Yohana Mbatizaji alikuja na hakula chakula cha kawaida au kunywa divai. Nanyi mkasema, ‘Ana pepo ndani yake.’ Mwana wa Adamu amekuja anakula na kunywa. Mnasema, ‘Mwangalieni anakula sana na kunywa sana divai. Ni rafiki wa watoza ushuru na watenda dhambi wengine.’ Lakini hekima huoneshwa kuwa sahihi kwa wale wanaoikubali.” Mmoja wa Mafarisayo alimwalika Yesu kula chakula nyumbani mwake. Yesu akaenda nyumbani kwa yule Farisayo, akaketi katika nafasi yake sehemu ya kulia chakula. Alikuwepo mwanamke mmoja katika mjini ule aliyekuwa na dhambi nyingi. Alipojua kuwa Yesu alikuwa anakula chakula nyumbani kwa Farisayo, alichukua chupa kubwa yenye manukato ya thamani sana. Alisimama karibu na miguu ya Yesu akilia. Kisha alianza kuisafisha miguu ya Yesu kwa machozi yake na akaifuta kwa nywele zake, akaibusu mara nyingi na kuipaka manukato. Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona hili, alijisemea moyoni mwake, “Mtu huyu angekuwa nabii, angetambua kuwa mwanamke huyu anayemgusa ni mwenye dhambi.” Katika kujibu kile Farisayo alichokuwa akifikiri, Yesu akasema, “Simoni nina kitu cha kukwambia.” Simoni akajibu, “Nieleze, Mwalimu.” Yesu akasema, “Kulikuwa watu wawili. Wote wawili walikuwa wanadaiwa na mkopeshaji mmoja. Mmoja alidaiwa sarafu mia tano za fedha, na wa pili sarafu hamsini za fedha. Watu wale hawakuwa na fedha, hivyo hawakuweza kulipa madeni yao. Lakini mkopeshaji aliwasamehe wote wawili. Kati ya wote wawili ni yupi atakayempenda mkopeshaji zaidi?” Simoni akajibu, “Nafikiri ni yule aliyekuwa anadaiwa fedha nyingi.” Yesu akamwambia, “Umejibu sawa.” Kisha akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, “Unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako hukunipa maji ili ninawe miguu yangu. Lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kuikausha kwa nywele zake. Wewe hukunisalimu kwa busu, lakini amekuwa akinibusu miguu yangu tangu nilipoingia. Hukuniheshimu kwa mafuta kwa ajili ya kichwa changu, lakini yeye amenipaka miguu yangu manukato yanayonukia vizuri. Ninakwambia kuwa dhambi zake zilizo nyingi zimesamehewa. Hii ni wazi, kwa sababu ameonesha upendo mkubwa. Watu wanaosamehewa kidogo hupenda kidogo.” Kisha akamwambia mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.” Watu waliokaa naye sehemu ya chakula wakaanza kusema mioyoni mwao, “Mtu huyu anadhani yeye ni nani? Anawezaje kusamehe dhambi?” Yesu akamwambia mwanamke, “Kwa sababu uliamini, umeokolewa kutoka katika dhambi zako. Nenda kwa amani.” Siku iliyofuata, Yesu alisafiri kupitia katika baadhi ya miji na vijiji. Yesu aliwahubiri watu Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Mitume kumi na wawili walikuwa pamoja naye. Walikuwepo pia baadhi ya wanawake ambao Yesu aliwaponya magonjwa na pepo wabaya. Mmoja wao alikuwa Mariamu aitwaye Magdalena ambaye alitokwa na pepo saba; Pia pamoja na wanawake hawa alikuwepo Yoana mke wa Kuza (msimamizi wa mali za Herode), Susana, na wanawake wengine wengi. Wanawake hawa walitumia fedha zao kuwahudumia Yesu na mitume wake. Kundi kubwa la watu lilikusanyika. Watu walimjia Yesu kutoka katika kila mji, naye Yesu akawaambia fumbo hili: “Mkulima alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akizitawanya, baadhi zilianguka kandokando ya njia. Watu wakazikanyaga, na ndege wa angani wakazila. Zingine zikaanguka kwenye udongo wenye mawe. Zilipoanza kukua zikafa kwa sababu ya kukosa maji. Mbegu zingine ziliangukia kwenye miiba. Miiba ikakua pamoja nazo, miiba ikazisongasonga na hazikukua. Zilizosalia ziliangukia kwenye udongo mzuri wenye rutuba. Mbegu hizi zikaota na kuzaa kila moja mia.” Yesu akamalizia fumbo. Kisha akapaza sauti, akasema, “Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni!” Wafuasi wake wakamwuliza, “Fumbo hili linamaanisha nini?” Akasema, “Mmechaguliwa kujua kweli za siri kuhusu ufalme wa Mungu. Lakini ninatumia mafumbo kuzungungumza na watu wengine. Ninafanya hivi ili, ‘Watazame, lakini wasiweze kuona. Wasikia, lakini wasielewe.’ Hii ndiyo maana ya fumbo hili: Mbegu ni Neno la Mungu. Watu wengine ni kama mbegu zilizoanguka njiani. Husikia mafundisho ya Mungu, lakini Shetani huja na kuwafanya waache kuyatafakari. Hii huwafanya kutoamini na kuokoka. Wengine wanafanana na mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye mawe. Ni watu ambao huyasikia mafundisho ya Mungu na kuyapokea kwa furaha, lakini kwa kuwa hawana mizizi yenye kina, huamini kwa muda mfupi. Majaribu yanapokuja, humwacha Mungu. Zilizoanguka katika miiba, zinafanana na watu wanaoyasikia Mafundisho ya Mungu, lakini wanaruhusu wasiwasi, mali na anasa za maisha haya kuwasimamisha na hawaendelei kukua. Hivyo mafundisho hayazalishi matokeo mazuri katika maisha yao. Na zile zilizoangukia katika udongo mzuri, ni wale ambao huyasikia mafundisho ya Mungu kwa moyo safi na mnyoofu. Huyatii na kwa uvumilivu wao huzaa mazao mazuri. Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa bakuli au kuificha uvunguni mwa kitanda. Badala yake huiweka kwenye kinara cha taa mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani wapate nuru ya kuwawezesha kuona. Kila jambo lililofichwa litawekwa wazi na kila siri itajulikana na kila mtu ataiona. Hivyo yatafakarini kwa umakini yale mnayosikia. Watu wenye uelewa kiasi watapokea zaidi. Lakini wale wasio na uelewa watapoteza hata ule wanaodhani kuwa wanao.” Mama yake Yesu na wadogo zake wakaenda kumwona, lakini walishindwa kumfikia kwa sababu walikuwepo watu wengi sana. Mtu mmoja akamwambia Yesu, “Mama yako na wadogo zako wamesimama nje. Wanataka kukuona.” Yesu akawajibu “Mama yangu na wadogo zangu ni wale wanaolisikia na kulitii Neno la Mungu.” Siku moja Yesu na wafuasi wake walipanda mashua. Akawaambia, “Tuvuke mpaka upande mwingine wa ziwa.” Wakaanza safari kuvuka ziwa. Walipokuwa wanasafiri, Yesu alisinzia. Tufani kubwa ikalikumba ziwa na mashua ikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari. Wafuasi wakamwendea, wakamwamsha, wakasema, “Mkuu, mkuu, tutazama!” Yesu akasimama, akaukemea upepo na mawimbi ya maji. Upepo ukakoma na ziwa likatulia. Ndipo Yesu akawaambia wafuasi wake, “Imani yenu iko wapi?” Lakini wao waliogopa na kustaajabu, wakanong'onezana, “Huyu ni mtu wa namna gani? Anaamuru upepo na maji, na vinamtii?” Yesu na wafuasi wake wakasafiri mpaka katika nchi walimoishi Wagerasi iliyokuwa ng'ambo ya ziwa Galilaya. Yesu alipotoka katika mashua, mwanaume mmoja kutoka katika mji ule alimwendea. Mtu huyu alikuwa na mapepo ndani yake. Kwa muda mrefu hakuwahi kuvaa nguo na aliishi makaburini. Pepo aliyekuwa ndani yake alikuwa akimpagaa mara nyingi na alikuwa akifungwa gerezani, mikono na miguu yake ikiwa imefungwa kwa minyororo. Lakini kila mara aliivunja. Pepo ndani yake alikuwa anamlazimisha kwenda nje ya mji mahali pasipoishi watu. Yesu alimwamuru kumtoka mtu yule. Alipomwona Yesu, alianguka mbele yake huku akipiga kelele kwa sauti, “Unataka nini kwangu, Yesu, Mwana wa Mungu Mkuu Aliye Juu? Tafadhali usiniadhibu!” *** Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?” Mtu yule akajibu, “Jeshi.” (Alisema jina lake ni “Jeshi” kwa sababu pepo wengi walikuwa wamemwingia.) Pepo wale wakamsihi Yesu asiwaamuru kwenda shimoni. Katika kilima kile, kulikuwa kundi kubwa la nguruwe wakichungwa. Pepo wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie wale nguruwe. Hivyo Yesu akawaruhusu. Pepo wakamtoka yule mtu, na kuwaingia nguruwe. Kundi lote la wale nguruwe likakimbia kutelemkia ziwani kwa kasi, nguruwe wakazama na kufia humo. Wachungaji wa nguruwe walipoona lililotokea, walikimbia, wakaenda kutoa taarifa mjini na mashambani. Watu wakaenda kuona lililotokea. Walipofika alipokuwa Yesu wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, akiwa na akili zake timamu; pepo walikuwa wamemtoka. Jambo hili likawaogopesha watu. Wale walioona mambo haya yalivyotokea waliwaambia wengine namna Yesu alivyomponya yule mtu. Watu wote waliokuwa wakiishi eneo lote la Gerasi wakamtaka Yesu aondoke kwa sababu waliogopa. Hivyo Yesu akapanda mashua na kurudi Galilaya. Mtu aliyeponywa alimsihi amfuate Yesu. Lakini Yesu akamtuma, akamwambia, “Rudi nyumbani, ukawaeleze watu mambo ambayo Mungu amekutendea.” Hivyo mtu yule alikwenda sehemu zote za mji akieleza mambo ambayo Yesu amemtendea. Yesu aliporudi Galilaya, watu walimkaribisha. Kila mtu alikuwa anamsubiri. Mtu mmoja jina lake Yairo, aliyekuwa mkuu wa sinagogi alimwendea. Alikuwa na binti mmoja tu mwenye umri wa miaka kumi na mbili na alikuwa mgonjwa sana katika hali ya kufa. Hivyo Yairo alisujudu miguuni pa Yesu na akamsihi aende nyumbani kwake. Yesu alipokuwa akienda nyumbani kwa Yairo, watu walimzonga kila upande. *** Mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili alikuwepo katika umati huo. Alikuwa ametumia mali zake zote kwa madaktari, lakini hakuna daktari aliyeweza kumponya. Alikwenda nyuma ya Yesu na kugusa pembe ya vazi lake. Wakati huo huo damu ikaacha kumtoka. Ndipo Yesu akasema, “Nani amenigusa?” Kila mtu alikataa kuwa hajamgusa, Petro akasema, “Mkuu, watu wamekuzunguka na wanakuzongazonga kila upande.” Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu amenigusa. Nimesikia nguvu ikinitoka.” Yule mwanamke alipoona ya kwamba hataweza kujificha akajitokeza akitetemeka. Akasujudu mbele ya Yesu. Huku kila mmoja akisikia, akaeleza sababu iliyomfanya amguse, na kwamba alipona wakati ule ule alipomgusa. Yesu alimwambia, “Binti yangu umeponywa kwa sababu uliamini. Nenda kwa amani.” Yesu alipokuwa bado anaongea, mtu mmoja kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi alikuja na akasema, “Binti yako amekwisha kufa! Hakuna haja ya kuendelea kumsumbua Mwalimu.” Yesu aliposikia maneno hayo, alimwambia Yairo, “Usiogope! Amini tu na binti yako ataponywa.” Yesu akaenda nyumbani, alipofika akaruhusu Petro, Yohana, Yakobo pamoja na baba na mama wa yule mtoto tu kuingia ndani pamoja naye. Kila mtu alikuwa akilia na kusikia huzuni kwa sababu msichana alikuwa amekufa. Lakini Yesu akasema, “Msilie. Hajafa. Amelala usingizi tu.” Watu wakamcheka, kwa sababu walijua kuwa amekwisha kufa. Lakini Yesu akamshika mkono na kumwambia, “Mtoto inuka!” Roho yake ikamrudia, akasimama hapo hapo. Yesu akasema, “Mpeni chakula.” Wazazi wa yule binti wakashangaa. Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote lililotokea. Yesu aliwaita mitume wake kumi na wawili pamoja, akawapa nguvu kuponya magonjwa na kutoa pepo kwa watu. Akawatuma kwenda kuhubiri kuhusu Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. Akawaambia, “Mnaposafiri, msibebe kitu chochote: msichukue fimbo ya kutembelea, msibebe mkoba, chakula au fedha. Chukueni nguo mlizovaa tu kwa ajili ya safari yenu. Mkiingia katika nyumba; kaeni katika nyumba hiyo mpaka mtakapokuwa mnatoka katika mji huo. Ikiwa watu katika mji mtakaoingia hawatawakaribisha, nendeni nje ya mji na kuyakung'uta mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.” Hivyo mitume wakaondoka. Walisafiri katika miji yote. Walihubiri Habari Njema na kuponya wagonjwa kila mahali. Herode, mtawala wa Galilaya alisikia mambo yote yaliyokuwa yanatokea. Alichanganyikiwa kwa sababu baadhi ya watu walisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka kwa wafu.” Wengine walisema, “Eliya amekuja kwetu,” na baadhi ya watu wengine walisema “Mmoja wa manabii wa kale amefufuka kutoka kwa wafu”. Herode alisema, “Nilimkata kichwa Yohana. Sasa, mtu huyu ninayesikia habari zake ni nani?” Herode aliendelea kutaka kumwona Yesu. Mitume waliporudi, walimwambia Yesu waliyoyafanya katika safari yao. Ndipo akawachukua mpaka kwenye mji uitwao Bethsaida. Ili yeye Yesu na mitume wawe peke yao pamoja. Lakini watu walipotambua mahali alikokwenda Yesu walimfuata. Aliwakaribisha na kuwaambia kuhusu ufalme wa Mungu. Na aliwaponya waliokuwa wagonjwa. Baadaye nyakati za jioni. Mitume kumi na mbili walimwendea na kumwambia, “Hakuna anayeishi mahali hapa. Waage watu. Wanahitaji kutafuta chakula na mahali pa kulala katika mashamba na miji iliyo karibu na eneo hili.” Lakini Yesu akawaambia mitume, “Wapeni chakula.” Wakasema, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu. Unataka twende tukanunue vyakula kwa ajili ya watu wote hawa? Ni wengi mno!” (Walikuwepo wanaume kama 5,000 pale.) Yesu akawaambia wafuasi wake, “Waambieni watu wakae katika vikundi vya watu hamsini hamsini.” Hivyo wafuasi wake wakafanya hivyo na kila mtu akakaa chini. Ndipo Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili. Akatazama juu mbinguni na kumshukuru Mungu kwa ajili ya chakula hicho. Kisha akaimega vipande vipande, akawapa wanafunzi wake ili wawape watu. Watu wote wakala mpaka wakashiba. Vikasalia vikapu kumi na mbili vilivyojaa vipande vya mikate na samaki ambavyo havikuliwa. Wakati mmoja Yesu alikuwa anaomba akiwa peke yake. Wafuasi wake walimwendea na aliwauliza, “Watu wanasema mimi ni nani?” Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine wanasema wewe ni Eliya, lakini wengine wanasema wewe ni mmoja wa manabii wa zamani aliyefufuka.” Kisha Yesu akawauliza wafuasi wake, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?” Petro akajibu, “Wewe ni Masihi kutoka kwa Mungu.” Yesu akawatahadharisha wasimwambie mtu yeyote. Yesu akasema, “Ni lazima Mwana wa Adamu apate mateso mengi. Nitakataliwa na viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Na nitauawa. Lakini siku ya tatu nitafufuliwa kutoka kwa wafu.” Kisha Yesu akamwambia kila mmoja aliyekuwa pale, “Mtu yeyote miongoni mwenu akitaka kuwa mfuasi wangu ni lazima ajikane yeye mwenyewe na mambo anayopenda. Ni lazima uubebe msalaba unaotolewa kwako kila siku kwa sababu ya kunifuata mimi. Yeyote miongoni mwenu anayetaka kuyaponya maisha yake atayaangamiza. Lakini yeyote atakayeyatoa maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa. Haina thamani kwenu kuupata ulimwengu wote ikiwa ninyi wenyewe mtateketezwa au kupoteza kila kitu. Msione aibu kwa sababu ya kunifuata na kusikiliza mafundisho yangu. Mkifanya hivyo, Mimi, Mwana wa Adamu, nitawaonea aibu nitakapokuja nikiwa na utukufu wangu, utukufu wa Baba na wa malaika watakatifu. Niaminini ninaposema kwamba baadhi yenu ninyi mliosimama hapa mtauona Ufalme wa Mungu kabla hamjafa.” Baada ya siku kama nane tangu Yesu aseme maneno haya, aliwachukua Petro, Yohana na Yakobo, akapanda mlimani kuomba. Yesu alipokuwa akiomba, uso wake ulianza kubadilika. Nguo zake zikawa nyeupe, zikang'aa. Kisha watu wawili walikuwa pale, wakiongea naye. Walikuwa Musa na Eliya; Wao pia walionekana waking'aa na wenye utukufu. Walikuwa wanazungumza na Yesu kuhusu kifo chake kitakachotokea Yerusalemu. Petro na wenzake walikuwa wanasinzia. Lakini waliamka na kuuona utukufu wa Yesu. Waliwaona pia watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. Musa na Eliya walipokuwa wanaondoka, Petro akasema, “Mkuu, ni vizuri tuko hapa. Tutajenga vibanda vitatu hapa, kimoja kwa ajili ya kukutukuza wewe, kingine kwa ajili kumtukuza Musa na kingine wa ajili ya kumtukuza Eliya.” Petro hakujua alichokuwa anasema. Petro alipokuwa akisema mambo haya, wingu likaja, likawafunika wote. Petro, Yohana na Yakobo waliogopa walipofunikwa na wingu. Sauti ikatoka katika wingu na kusema, “Huyu ni Mwanangu. Ndiye niliyemchagua. Mtiini yeye.” Sauti hiyo ilipomalizika, Yesu peke yake ndiye alikuwa pale. Petro, Yohana na Yakobo hawakusema chochote. Na kwa muda mrefu baada ya hilo, hawakumwambia mtu yeyote yale waliyoyaona. Siku iliyofuata, Yesu, Petro, Yohana na Yakobo walitelemka kutoka mlimani. Kundi kubwa la watu likaenda kukutana naye. Mtu mmoja katika umati huo alimwita Yesu akisema, “Mwalimu, tafadhali njoo umwonee mwanangu. Ni mtoto pekee niliye naye. Pepo mchafu humvaa na hupiga kelele, humtia kifafa na kumtoa povu mdomoni. Huendelea kumwumiza na hamwachi kirahisi. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe pepo huyu mchafu lakini wameshindwa.” Yesu akajibu, “Enyi watu msio na imani. Maisha yenu ni mabaya. Nitakaa na kuchukuliana nanyi mpaka lini?” Ndipo Yesu akamwambia yule mtu, “Mlete kijana wako hapa.” Kijana alipokuwa anakwenda kwa Yesu, pepo mchafu akamwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamwamuru atoke. Kijana akaponywa, na Yesu akampeleka kwa baba yake. Watu wote wakaushangaa ukuu wa nguvu ya Mungu. Watu walipokuwa bado wanayashangaa mambo yote aliyofanya Yesu. Akawaambia wanafunzi wake, “Msiyasahau nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu yu karibu kukamatwa na kuwekwa katika mikono ya watu wengine.” Lakini wanafunzi hawakuelewa alichomaanisha. Maana ilifichwa kwao ili wasitambue. Lakini waliogopa kumwuliza Yesu kuhusiana na alilosema. Wafuasi wa Yesu walianza kubishana wakiulizana nani ni mkuu kuliko wote miongoni mwao. Yesu alijua walichokuwa wanafikiri, hivyo akamchukua mtoto mdogo na kumsimamisha karibu yake. Kisha akawaambia, “Yeyote anayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu kwa jina langu ananikaribisha mimi. Na yeyote anayenikaribisha mimi anamkaribisha yule aliyenituma. Aliye mnyenyekevu zaidi miongoni mwenu, ndiye mkuu.” Yohana akajibu; “Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kutoka kwa watu akitumia jina lako. Tulimwambia aache kwa sababu hayuko katika kundi letu.” Yesu akamwambia, “Msimkataze. Asiye kinyume nanyi yu pamoja nanyi.” Wakati ulikuwa unakaribia ambapo Yesu alikuwa aondoke na kurudi mbinguni. Hivyo aliamua kwenda Yerusalemu. Alituma baadhi ya watu kumtangulia. Waliondoka na kwenda katika mji mmoja wa Samaria, ili kumwandalia mahali pa kufikia. Lakini watu katika mji huo hawakumkaribisha Yesu kwa sababu alikuwa anakwenda Yerusalemu. Wafuasi wake; Yakobo na Yohana walipoona hayo, wakasema, “Bwana, unataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni na kuwateketeza watu hawa?” Lakini Yesu aligeuka na akawakemea baada ya wao kusema hivi. Kisha Yesu na wanafunzi wake wakaondoka wakaenda katika mji mwingine. Walipokuwa wakisafiri pamoja njiani, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata kokote utakakokwenda.” Yesu akamwambia, “Mbweha wana mapango na ndege wa angani wana viota. Lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.” Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate!” Lakini mtu yule akamwambia, “Bwana, niache nikamzike baba yangu kwanza.” Lakini Yesu akamwambia, “Waache waliokufa wawazike wafu wao. Ni lazima uende kuhubiri kuhusu Ufalme wa Mungu.” Mtu mwingine pia akamwambia, “Nitakufuata Bwana, lakini niruhusu kwanza nikaiage familia yangu.” Yesu akamwambia, “Mtu yeyote anayeanza kulima, kisha akaangalia nyuma hajajiandaa kwa ajili ya Ufalme wa Mungu.” Baada ya hili, Bwana alichagua wafuasi sabini na wawili zaidi. Aliwatuma watangulie katika kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda wakiwa wawili wawili. Aliwaambia, “Kuna mavuno mengi ya watu wa kuwaingiza katika Ufalme wa Mungu. Lakini watenda kazi wa kuwaingiza katika ufalme wa Mungu ni wachache. Mungu anamiliki mavuno. Mwombeni ili atume watenda kazi wengi ili wasaidie kuyaingiza mavuno yake. Mnaweza kwenda sasa. Lakini sikilizeni! Ninawatuma na mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Msibebe mfuko wowote, wala pesa au viatu. Msisimame kusalimiana na watu njiani. Kabla ya kuingia katika nyumba, mseme, ‘Amani iwemo katika nyumba hii.’ Ikiwa watu wanaoishi katika nyumba hiyo wanapenda amani, baraka yenu ya amani itakaa nao. Lakini kama siyo, baraka yenu ya amani itawarudia. Kaeni katika nyumba inayopenda amani. Kuleni na kunywa chochote watakachowapa kwa maana mfanyakazi anastahili ujira. Msihame kutoka katika nyumba hiyo na kwenda kukaa katika nyumba nyingine. Mkiingia katika mji wowote na watu wakawakaribisha, kuleni vyakula watakavyowapa. Waponyeni wagonjwa wanaoishi katika mji huo, na waambieni Ufalme wa Mungu umewafikia! Lakini mkiingia katika mji wowote na watu wasiwakaribishe, nendeni katika mitaa ya mji huo na mseme, ‘Tunafuta mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana katika miguu yetu! Lakini kumbukeni kwamba: Ufalme wa Mungu umewafikia!’ Ninawaambia, siku ya hukumu itakuwa vibaya sana kwa watu wa mji huo kuliko watu wa Sodoma. Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Watu wenu wameniona nikifanya miujiza mingi ndani yenu, lakini hamkubadilika. Miujiza hiyo hiyo ingefanyika katika miji ya Tiro na Sidoni, watu katika miji hiyo wangelikwisha badili mioyo na maisha yao siku nyingi. Wangelikwisha vaa nguo za magunia na kukaa kwenye majivu kuonesha kusikitika na kutubu dhambi zao. Lakini itakuwa rahisi kwa miji ya Tiro na Sidoni siku ya hukumu kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, Je! Utatukuzwa mpaka mbinguni? Hapana, utatupwa chini hadi mahali pa kifo. Mtu yeyote akiwasikiliza ninyi wafuasi wangu, hakika ananisikiliza mimi. Lakini mtu yeyote akiwakataa ninyi, hakika ananikataa mimi. Na mtu yeyote akinikataa mimi anamkataa Yule aliyenituma.” Wale wafuasi sabini na wawili waliporudi kutoka katika safari yao, walikuwa na furaha sana. Walisema, “Bwana, hata pepo walitutii tulipotumia jina lako!” Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kama mwanga wa radi kutoka mbinguni! Yeye ndiye adui, lakini tambueni kuwa nimewapa mamlaka zaidi yake. Nimewapa mamlaka ya kuponda nyoka na nge zake kwa miguu yenu. Hakuna kitakachowadhuru. Ndiyo, hata pepo wanawatii. Na mnaweza kufurahi, lakini si kwa sababu mna mamlaka hii. Furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” Ndipo Yesu akajisikia furaha kwa uweza wa Roho Mtakatifu, akasema, “Ninakusifu wewe, Baba, BWANA wa mbingu na nchi. Ninashukuru kwamba umewaficha mambo haya wenye hekima na akili nyingi. Lakini umeyafunua kwa watu walio kama watoto wadogo. Ndiyo, Baba, umefanya hivi kwa sababu hakika ndivyo ulitaka kufanya. Baba yangu amenipa vitu vyote. Hakuna anayejua Mwana ni nani, Baba peke yake ndiye anayejua. Na Mwana peke yake ndiye anayejua Baba ni nani. Watu pekee watakaojua kuhusu Baba ni wale ambao Mwana amechagua kuwaambia.” Wafuasi walikuwa na Yesu peke yao na Yesu aliwageukia akasema, “Ni baraka kubwa kwenu kuyaona mnayoyaona sasa! Ninawaambia, Manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mambo haya mnayoyaona ninyi, lakini hawakuyaona, na walitamani kuyasikia mnayoyasikia ninyi lakini hawakuweza.” Kisha mwanasheria mmoja alisimama ili amjaribu Yesu. Akasema, “Mwalimu, ninatakiwa nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Yesu akamwambia, “Imeandikwa nini katika torati? Unaielewaje?” Yule mwana sheria akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote.’ Pia ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’” Yesu akasema, “Jibu lako ni sahihi. Fanya hivi nawe utaupata uzima wa milele.” Lakini mwanasheria alitaka kuonesha kuwa alikuwa mwenye haki na aliishi kwa usahihi. Hivyo akamwuliza Yesu, “Lakini si kila mtu aliye jirani yangu, au unasemaje?” Katika kujibu swali hili, Yesu akasema, “Mtu mmoja alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Akiwa njiani alivamiwa na majambazi, wakamchania nguo na kumpiga. Kisha wakamwacha amelala chini akiwa katika hali ya kufa. Ikatokea kuwa kuhani mmoja alikuwa anasafiri kupitia njia hiyo hiyo. Alipomwona, hakusimama ili amsaidie, alikwenda zake. Kisha Mlawi alipokaribia na kumwona yule mtu, alipita upande mwingine. Hakusimama ili amsaidie, Alikwenda zake. Ndipo Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri kupitia njia ile ile, alipofika mahali ambapo mtu aliyejeruhiwa alikuwa amelala, alipomwona alimhurumia. Alimkaribia ili amsaidie, akamsafisha majeraha kwa mafuta ya zeituni na divai, kisha akayafunga majeraha yake. Msamaria alikuwa na punda. Akampandisha juu ya punda wake na kumpeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni. Akamhudumia huko. Siku iliyofuata, Msamaria alitoa sarafu mbili za fedha na kumpa mtunza nyumba ya wageni, akamwambia, ‘Mtunze mtu huyu aliyejeruhiwa. Ukitumia pesa nyingi zaidi kwa kumhudumia, nitakulipa nitakapokuja tena.’” Kisha Yesu akasema, “Ni yupi kati ya hawa watu watatu unadhani hakika alikuwa jirani wa yule mtu aliyepigwa na majambazi?” Mwanasheria akajibu, “Ni yule aliyemsaidia.” Yesu akasema, “Basi nenda ukafanye kama alivyofanya.” Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanasafiri, walifika katika kijiji kimoja. Mwanamke aitwaye Martha alimkaribisha nyumbani kwake. Alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Mariamu. Mariamu alikuwa amekaa karibu na Yesu akimsikiliza anavyofundisha. Lakini Martha dada yake Mariamu alikuwa anashughulisha na shughuli mbalimbali zilizotakiwa kufanywa. Martha aliingia ndani na akasema, “Bwana, hujali kuona mdogo wangu ameniacha nifanye kazi zote peke yangu? Mwambie aje kunisaidia.” Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, unasumbuka na kuhangaika kwa shughuli nyingi. Lakini kitu kimoja tu ndicho cha lazima. Mariamu amefanya uchaguzi sahihi na kamwe hautachukuliwa kutoka kwake.” Siku moja Yesu alitoka akaenda mahali fulani kuomba. Alipomaliza, mmoja wa wafuasi wake akamwambia, “Yohana aliwafundisha wafuasi wake namna ya kuomba. Bwana, tufundishe nasi pia.” Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivi ndivyo mnapaswa kuomba: ‘Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe daima. Tunaomba Ufalme wako uje. Utupe chakula tunachohitaji kila siku. Utusamehe dhambi zetu, kama tunavyomsamehe kila mtu anayetukosea. Na usiruhusu tukajaribiwa.’” Kisha Yesu akawaambia, “Chukulia mmoja wenu angekwenda kwa rafiki yake usiku na kumwambia, ‘Rafiki yangu aliyekuja mjini amekuja kunitembelea. Lakini sina chakula cha kumpa ili ale. Tafadhali nipe mikate mitatu.’ *** Rafiki yako ndani ya nyumba akajibu, ‘Nenda zako! Usinisumbue! Mlango umefungwa. Mimi na watoto wangu tumeshapanda kitandani kulala. Siwezi kuamka ili nikupe kitu chochote kwa sasa.’ Ninawaambia, urafiki unaweza usimfanye aamke akupe kitu chochote. Lakini hakika ataamka ili akupe unachohitaji ikiwa utaendelea kumwomba. Hivyo ninawaambia, Endeleeni kuomba na Mungu atawapa. Endeleeni kutafuta na mtapata. Endeleeni kubisha milangoni, na milango itafunguliwa kwa ajili yenu. Ndiyo, kila atakayeendelea kuomba atapokea. Kila atakayeendelea kutafuta atapata. Na kila atakayeendelea kubisha mlangoni, mlango utafunguliwa kwa ajili yake. Je, kuna mmoja wenu aliye na mwana? Utafanya nini ikiwa mwanao atakuomba samaki? Je, kuna baba yeyote anayeweza kumpa nyoka? Au akiomba yai, utampa nge? Hakika hakuna baba wa namna hivyo. Ikiwa ninyi waovu mnajua namna ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri. Vivyo hivo, hakika Baba yenu aliye mbinguni anajua namna ya kuwapa Roho Mtakatifu wale wanao mwomba?” Wakati mmoja Yesu alikuwa akitoa pepo aliyemfanya mtu ashindwe kuzungumza. Ikawa, pepo alipotoka, yule mtu akaanza kuongea, umati wa watu walishangaa. Lakini baadhi ya watu walisema, “Anatumia nguvu za Shetani kuwatoa pepo. Shetani ni mtawala wa pepo wachafu.” Baadhi ya watu wengine waliokuwa pale walitaka kumjaribu Yesu, walimwomba afanye muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini alijua walichokuwa wanafikiria, hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe huteketezwa; na familia yenye magomvi husambaratika. Hivyo, ikiwa Shetani anapigana yeye mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Ninawauliza hivi kwa kuwa mnasema kwamba ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani. Lakini ikiwa ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani, watu wenu wanatumia nguvu gani wanapotoa pepo? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa ninyi ni waovu. Lakini, ninatumia nguvu za Mungu kutoa pepo. Hii inaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu sasa. Mwenye nguvu aliye na silaha nyingi anapoilinda nyumba yake, vitu vilivyomo ndani ya nyumba yake huwa salama. Lakini chukulia kuwa mwenye nguvu zaidi kuliko yeye akimshambulia na kumshinda, yule mwenye nguvu zaidi humnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea kuilinda nyumba yake. Ndipo mwenye nguvu zaidi atavitumia vitu vya yule mtu wa kwanza kadri anavyotaka. Mtu yeyote asiye pamoja nami, yuko kinyume nami. Na mtu yeyote asiyefanya kazi pamoja nami anafanya kinyume nami. Mtu anapotokwa na roho chafu, roho hiyo husafiri sehemu zilizo kavu, ikitafuta mahali ili ipumzike. Lakini hukosa mahali pa kupumzika. Hivyo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba nilikotoka.’ Inaporudi hukuta nyumba imesafishwa na kupangwa vizuri. Ndipo roho hiyo chafu huenda ikachukua roho wengine saba, walio waovu kuliko yenyewe. Na kwa pamoja roho zote hizo huingia na kuishi ndani ya mtu huyo, na mtu huyo hupata matatizo mengi kuliko ya kwanza.” Yesu alipokuwa akisema mambo haya, mwanamke mmoja katika kundi la watu akapaza sauti akamwambia “Amebarikiwa na Mungu mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!” Lakini Yesu akasema, “Wamebarikiwa zaidi wanaosikia na kuyatii mafundisho ya Mungu.” Baada ya kundi la watu kuongezeka na kumzunguka, Yesu alisema, “Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu. Mnaomba muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia jambo lolote. Ishara pekee mtakayopata ni kile kilichompata Yona. Yona alikuwa ishara kwa watu walioishi katika mji wa Ninawi. Ni sawasawa na Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa watu wa wakati huu. Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa, mtalinganishwa na Malkia wa Kusini, naye pia, atakuwa shahidi atakayeonyesha namna mlivyo waovu. Kwa nini ninasema haya? Kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana ili ayasikilize mafundisho yenye hekima ya Suleimani. Na ninawaambia mkuu kuliko Suleimani yupo hapa, lakini hamnisikilizi! Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa mtafananishwa pia na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha makosa yenu. Ninasema hivi kwa sababu Yona alipowahubiri, walibadili mioyo na maisha yao. Na sasa mnamsikia mtu aliye mkuu kuliko Yona, Lakini hamtaki kubadilika! Hakuna mtu anayechukua taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunika. Badala yake huiweka mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani waweze kuiona nuru yake. Namna unavyowatazama watu inaonesha kwa hakika jinsi ulivyo. Unapowatazama watu katika hali isiyo ya ubinafsi, inaonesha wazi kuwa umejaa nuru. Lakini unapowatazama watu katika namna ya uchoyo, ni wazi kuwa umejaa giza. Hivyo iweni waangalifu ili nuru iliyo ndani yenu usiwe giza! Ikiwa umejaa nuru na hakuna sehemu yenye giza ndani yako, basi utang'aa, kama nuru ya kwenye taa.” Baada ya Yesu kumaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika Yesu kula pamoja naye. Hivyo Yesu alikwenda na kuketi sehemu ya kulia chakula. Lakini Farisayo alishangaa alipoona Yesu hakunawa mikono yake kwanza kabla ya kuanza kula. Bwana akamwambia, “Usafi mnaoufanya ninyi Mafarisayo ni kama kusafisha kikombe au sahani kwa nje tu. Lakini ndani yenu mna nini? Mnataka kuwadanganya na kuwaumiza watu tu. Ninyi ni wajinga! Aliyeumba kilicho nje ndiye aliumba kilicho ndani. Hivyo, jalini vilivyo ndani. Wapeni vitu wenye uhitaji. Ndipo mtakuwa wasafi kikamilifu. Lakini, ole wenu ninyi Mafarisayo! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya vyakula mnavyopata, hata mnanaa, na hata kila mmea mdogo katika bustani zenu. Lakini mnapuuzia kuwatendea haki wengine na kumpenda Mungu. Haya ni mambo mnayotakiwa kufanya. Na endeleeni kufanya mambo hayo mengine. Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kupata viti vya heshima katika masinagogi. Na mnapenda kusalimiwa na watu kwa kuheshimiwa sehemu za masoko. Ole wenu, kwa kuwa mnafanana na makaburi ya zamani yasiyoonekana, ambayo watu hupita juu yake na kuyakanyaga bila kuyatambua.” Mmoja wa wanasheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, unaposema mambo haya kuhusu Mafarisayo unatukosoa hata sisi pia.” Yesu akamjibu, “Ole wenu, enyi wanasheria! Mnatunga sheria kali ambazo ni vigumu watu kuzitii. Mnawalazimisha wengine kuzitii sheria zenu. Lakini ninyi wenyewe hamthubutu hata kujaribu kufuata mojawapo ya sheria hizo. Ole wenu kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii. Lakini hawa ni manabii wale wale ambao mababu zenu waliwaua. Na sasa mnawaonesha watu wote kwamba mnakubaliana na mambo ambayo baba zenu walifanya. Waliwaua manabii, nanyi mnasherehekea mauaji hayo kwa kujenga makaburi ya manabii! Hii ndiyo sababu ambayo kwa Hekima yake Mungu alisema, ‘Nitawatuma manabii na mitume kwao. Baadhi ya manabii na mitume wangu watauawa na watu waovu. Wengine watateswa sana.’ Hivyo ninyi watu mnaoishi sasa mtaadhibiwa kwa sababu ya vifo vya manabii wote waliouawa tangu mwanzo wa ulimwengu. Mtachukuliwa wenye hatia kutokana na vifo hivyo vyote, tangu kuuawa kwa Habili mpaka kuuawa kwa nabii Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na Hekalu. Ndiyo ninawaambia, kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu yao wote. Ole wenu, ninyi wanasheria, mmechukua ufunguo wa kujifunza kuhusu Mungu. Ninyi wenyewe hamtaki kujifunza na mmewazuia wengine wasijifunze pia.” Yesu alipotoka humo, walimu wa sheria na Mafarisayo walianza kumpinga sana. Walianza kumjaribu ili awajibu maswali kuhusu mambo mengi, ili Yesu akisema jambo isivyo sahihi waweze kupata sababu ya kumkosoa. Maelfu wengi wa watu walikusanyika. Walikuwepo watu wengi sana kiasi ambacho walikuwa wakikanyagana. Kabla Yesu hajaanza kuzungumza na watu wale, aliwaambia wafuasi wake, “Iweni waangalifu dhidi ya chachu ya Mafarisayo. Ninamaanisha kuwa hao ni wanafiki. Kila kitu kilichofichwa kitawekwa wazi, na kila kitu kilicho sirini kitajulikana. Mnachokisema sirini kitasemwa mbele za watu. Na mliyonong'onezana katika vyumba vyenu, yatahubiriwa sehemu za wazi ambako kila mtu atasikia.” Kisha Yesu akawaambia watu, “Ninawaambia ninyi, rafiki zangu, msiwaogope watu. Wanaweza kuua mwili, lakini baada ya hilo hawawezi kufanya chochote cha kuwaumiza. Mwogopeni Mungu maana Yeye ndiye mwenye nguvu ya kuwaua na kuwatupa Jehanamu. Ndiyo, mnapaswa kumwogopa yeye. Ndege wanapouzwa, ndege watano wadogo wanagharimu senti mbili tu za shaba. Lakini Mungu hasahau hata mmoja wao. Ndiyo, Mungu anajua hata idadi ya nywele mlizonazo kwenye vichwa vyenu. Msiogope ninyi ni wa thamani kuliko ndege wengi. Ninawaambia, mkinikiri mbele za watu, ndipo nami nitakiri kuwa ninyi ni wangu mbele za Mungu na malaika. Na atakayenikataa mimi mbele za watu, nami nitamkataa mbele za Mungu na malaika. Kila asemaye neno kinyume na Mwana wa Adamu atasamehewa. Lakini atakayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa. Watakapowapeleka ninyi katika masinagogi mbele ya viongozi na wenye mamlaka, msihangaike mtasema nini. Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.” Mmoja wa watu katika kundi akamwambia Yesu, “Mwalimu, baba yetu amefariki hivi karibuni na ametuachia vitu, mwambie kaka yangu anigawie baadhi ya vitu hivyo!” Lakini Yesu akamwambia, “Nani amesema mimi ni mwamuzi wa kuwaamulia namna ya ninyi wawili kugawana vitu vya baba yenu?” Ndipo Yesu akawaambia, “Iweni waangalifu na jilindeni dhidi ya kila aina ya ulafi. Maana uhai wa watu hautokani na vitu vingi wanavyomiliki.” Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Alikuwepo tajiri mmoja aliyekuwa na shamba. Shamba lake lilizaa mazao sana. Akasema moyoni mwake, ‘Nitafanya nini? Sina mahali pa kuyaweka mazao yangu yote?’ Kisha akasema, ‘Ninajua nitakachofanya. Nitabomoa ghala zangu na kujenga ghala kubwa zaidi! Nitahifadhi nafaka zangu zote na vitu vingine vizuri katika ghala zangu mpya. Kisha nitajisemea mwenyewe, nina vitu vingi vizuri nilivyotunza kwa ajili ya kutumia kwa miaka mingi ijayo. Pumzika, kula, kunywa na furahia maisha!’ Lakini Mungu akamwambia yule mtu, ‘Ewe mpumbavu! Leo usiku utakufa. Sasa vipi kuhusu vitu ulivyojiandalia? Nani atavichukua vitu hivyo?’ Hivi ndivyo itakavyokuwa kwa mtu anayeweka vitu kwa ajili yake yeye peke yake. Mtu wa namna hiyo si tajiri kwa Mungu.” Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivyo ninawaambia, msisumbuke juu ya vitu mnavyohitaji kwa ajili ya kuishi, mtakula nini au mtavaa nini. Maisha ni muhimu zaidi ya chakula mnachokula na mwili ni zaidi ya mavazi mnayovaa. Waangalieni kunguru, hawapandi, hawavuni au kuweka katika majumba au ghala, lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani sana kuliko ndege. Hakuna mmoja wenu anayeweza kujiongezea muda katika maisha yake kwa kujihangaisha na maisha. Na ikiwa hamwezi kufanya mambo madogo, kwa nini mnajihangaisha kwa mambo makubwa? Yatafakarini maua yanavyoota. Hayafanyi kazi wala kujitengenezea mavazi. Lakini ninawaambia hata Sulemani, mfalme mkuu na tajiri, hakuvikwa vizuri kama maua haya. Ikiwa Mungu huyavika vizuri namna hii majani ya porini, mnadhani atawafanyia nini ninyi? Hilo ni jani tu, siku moja li hai na siku inayofuata linachomwa moto. Lakini Mungu huyajali kiasi cha kuyapendezesha. Hakika atafanya zaidi kwa ajili yenu. Imani yenu ni ndogo! Hivyo daima msijihangaishe na kile mtakachokula ama mtakachokunywa. Msisumbukie mambo haya. Hayo ndiyo mambo ambayo watu wote wasiomjua Mungu huyafikiria daima. Lakini Baba yenu anajua ya kuwa mnayahitaji mambo haya. Mnapaswa kufikiri kuhusu ufalme wa Mungu. Naye Mungu atawapa mambo mengine yote mnayohitaji. Msiogope, enyi kundi dogo. Kwa kuwa imempendeza Baba yenu kuwapa ninyi ufalme wake. Uzeni vitu mlivyo navyo, wapeni fedha wale wanaohitaji. Hii ni njia pekee mnayoweza kufanya utajiri wenu usipotee. Mtakuwa mnaweka hazina isiyoisha mbinguni, mahali ambapo wezi hawawezi kuiba na hakuna wadudu wa kuharibu. Kwa kuwa mahali ilipo hazina yako, ndipo roho yako itakapokuwa. Iweni tayari! Vaeni kikamilifu na taa zenu zikiwaka. Iweni tayari kama watumishi wanaomngojea bwana wao anayerudi kutoka kwenye sherehe ya harusi. Bwana wao anaporudi na kubisha mlangoni, watumishi huweza kumfungulia mlango haraka. Bwana wao atakapoona kuwa wako tayari na wanamsubiri, itakuwa siku ya furaha kwa watumishi hao. Ninawaambia bila mashaka, bwana wao atavaa nguo, atawakaribisha kwenye chakula kisha atawahudumia. Watumishi hao wanaweza kumsubiri bwana wao mpaka usiku wa manane. Lakini watafurahi sana kwa sababu aliporudi aliwakuta bado wanamsubiri. Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua ni lini mwizi atakuja? Mnajua kuwa asingeruhusu mwizi akavunja na kuingia ndani. Hivyo, iweni tayari ninyi nanyi, kwa kuwa Mwana wa Adamu atakuja wakati msiotarajia!” Petro akasema, “Bwana, mfano ule ulikuwa kwa ajili yetu au kwa ajili ya watu wote?” Bwana akamjibu, “Fikiria kuhusu mtumishi mwenye hekima na mwaminifu, ambaye bwana wake anamwamini na kumweka kuwa msimamizi wa kuwapa watumishi wengine chakula kwa wakati uliokubalika? Mtumishi huyo ataoneshaje kuwa yeye ni msimamizi makini na anayeweza kujisimamia? Mkuu wake atakaporudi na kumkuta akifanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha sana kwa mtumishi huyo. Ninawaambia ukweli bila mashaka yo yote, mkuu wake atamweka kuwa msimamizi wa vitu vyake vyote anavyomiliki. Lakini itakuwaje ikiwa mtumishi huyo ni mwovu na akadhani bwana wake hatarudi mapema? Ataanza kuwapiga watumishi wengine, wanaume na wanawake. Atakula na kunywa mpaka atalewa. Ndipo bwana wa mtumishi huyo atakuja wakati usiotarajiwa, wakati ambapo mtumishi hajajiandaa. Ataadhibiwa bila huruma na bwana wake na kumpeleka anakostahili, mahali waliko watumishi wengine wasiotii. Mtumishi huyo alijua kitu ambacho bwana wake alimtaka afanye. Lakini hakuwa tayari kufanya au kujaribu kufanya kile bwana wake alichotaka. Hivyo mtumishi huyo ataadhibiwa sana! Lakini vipi kuhusu mtumishi asiyejua kile ambacho bwana wake anataka? Yeye pia anafanya mambo yanayostahili adhabu, lakini ataadhibiwa kidogo kuliko mtumishi aliyejua alichotakiwa kufanya. Yeyote aliyepewa vingi atawajibika kwa vingi. Hivyo vingi vitategemewa kutoka kwa yule aliyepewa vingi zaidi.” Yesu aliendelea kusema: “Nimekuja kuleta moto ulimwenguni. Ninatamani ungekuwa unawaka tayari! Kuna aina ya ubatizo ambao ni lazima niupitie na niteseke. Ninajisikia kusumbuka mpaka pale utakapotimizwa. Mnadhani nilikuja kuleta amani ulimwenguni? Hapana, nilikuja kuugawa ulimwengu! Kuanzia sasa, familia ya watu watano itagawanyika, watatu watakuwa kinyume cha wawili, na wawili kinyume cha watatu. Kina baba watakuwa kinyume cha wana wao: na wana nao watakuwa kinyume cha baba zao. Kina mama watakuwa kinyume cha binti zao: na binti nao watakuwa kinyume cha mama zao. Mama wakwe watakuwa kinyume cha wake za wana wao, na wake za wana wao watakuwa kinyume cha mama wakwe zao.” Ndipo Yesu akawaambia watu, “Mnapoona wingu likikua upande wa magharibi, mnasema, ‘Mvua inakuja,’ na muda si mrefu huanza kunyesha. Mnapoona upepo unaanza kuvuma kutoka kusini mnasema, ‘Kutakuwa joto,’ na huwa hivyo. Enyi wanafiki! Mnaweza kuiona nchi na anga na mkajua hali ya hewa itakavyokuwa. Kwa nini hamwelewi kinachotokea sasa? Kwa nini ninyi wenyewe hamwezi kujiamulia ninyi wenyewe kilicho haki? Ikiwa mtu anakushtaki na ninyi nyote mnaongozana kwenda mahakamani. Jitahidi kadri inavyowezekana kupatana naye mkiwa njiani. Usipopatana naye, atakupeleka kwa hakimu. Na hakimu atakutia hatiani na maofisa wa mahakama watakutupa gerezani. Ninawaambieni, hautatoka humo, mpaka ulipe kila senti unayodaiwa.” Sehemu ya watu waliokuwa pamoja na Yesu pale, walimweleza kilichowapata baadhi ya waabuduo kutoka Galilaya. Pilato alikuwa ameamuru wauawe. Damu zao zilichanganywa na damu za wanyama waliowaleta kwa ajili ya kutoa dhabihu. Yesu alijibu akasema, “Mnadhani hili liliwapata watu hao kwa sababu walikuwa wenye dhambi kuliko watu wengine wote wa Galilaya? Hapana, hawakuwa hivyo. Lakini ikiwa hamtaamua kubadili maisha yenu sasa, ninyi nyote mtaangamizwa kama wao! Na vipi kuhusu wale watu kumi na wanane waliokufa pale mnara wa Siloamu ulipowaangukia? Mnadhani walikuwa na dhambi kuliko watu wengine katika mji wa Yerusalemu? Hawakuwa hivyo. Lakini ninawaambia, ikiwa hamtaamua kubadilika sasa, hata ninyi mtaangamizwa pia!” Yesu akawasimulia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa amepanda mtini katika shamba lake. Alipokuja kutafuta matunda kwenye mtini huo hakupata tunda lolote. Alikuwa na mtumishi aliyekuwa akilitunza shamba. Hivyo alimwambia mtumishi wake, ‘Nimekuwa nikitafuta matunda kwenye mti huu kwa miaka mitatu, lakini sijawahi kupata tunda lolote. Ukate mti huu! Kwa maana unaiharibu ardhi.’ Lakini mtumishi alijibu, ‘Mkuu, tuuache mti huu mwaka mmoja zaidi ili tuone ikiwa utazaa matunda. Nitakusanya samadi kuuzunguka ili kuupa mbolea. Unaweza kuzaa matunda mwaka ujao. Ikiwa hautazaa, ndipo utaweza kuukata.’” Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi moja siku ya Sabato. Alikuwepo mwanamke mmoja ndani ya sinagogi aliyekuwa na pepo mchafu aliyemlemaza kwa muda wa miaka kumi na nane. Mgongo wake ulikuwa umepinda na hakuweza kusimama akiwa amenyooka. Yesu alipomwona alimwita na kumwambia, “Mama, umefunguliwa kutoka katika ugonjwa wako!” Akaweka mikono yake juu yake na saa hiyo hiyo akaweza kusimama akiwa amenyooka. Akaanza kumsifu Mungu. Kiongozi wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu aliponya siku ya Sabato. Akawaambia watu, “Kuna siku sita za kufanya kazi. Hivyo njooni ili mponywe katika moja ya siku hizo, msije siku ya Sabato kutafuta uponyaji.” Yesu akamjibu kwa kusema, “Ninyi watu ni wanafiki! Ninyi nyote huwafungulia punda au ng'ombe wenu wa kulimia kutoka zizini na kuwapeleka kunywa maji kila siku, hata siku ya Sabato. Mwanamke huyu niliyemponya ni mzaliwa halisi wa Ibrahimu. Lakini Shetani alikuwa amemfunga kwa miaka kumi na nane. Hakika si kosa yeye kuponywa ugonjwa wake siku ya Sabato!” Yesu aliposema haya, watu wote waliokuwa wanampinga walidhalilika. Kundi lote likafurahi kwa sababu ya mambo makuu aliyatenda. Kisha Yesu akasema, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Niufananishe na nini? Ufalme wa Mungu ni kama mbegu ya haradali. Mtu mmoja aliichukua na kuipanda katika bustani yake. Mbegu ikaota, ikakua na kuwa mti na ndege wakatengeneza viota kwenye matawi yake.” Yesu akasema tena, “Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Ufalme wa Mungu unafanana na kiasi kidogo cha chachu ambacho mwanamke hutumia kuchanganya na kilo 20 za unga kutengeneza mkate. Hamira huumua kinyunya chote.” Yesu alikuwa akifundisha katika kila mji na kijiji. Aliendelea kusafiri kuelekea Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, “Bwana, watu wangapi wataokolewa? Ni wachache?” Yesu akajibu, “Mlango wa kuingia katika ufalme wa Mungu ni mwembamba. Jitahidini kuingia kupitia mlango huo. Watu wengi watataka kuingia huko, lakini hawataweza. Mtu anapoufunga mlango wa nyumba yake, unaweza ukasimama nje na kubisha mlangoni, lakini hataufungua. Mnaweza kusema, ‘Mkuu tufungulie mlango!’ Lakini yeye akawajibu, ‘Siwajui ninyi na mnakotoka sikujui.’ Ndipo mtaanza kusema, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe. Ulifundisha katika mitaa ya mji wetu.’ Kisha atawaambia, ‘Siwajui na sijui mlikotoka! Ondokeni kwangu! Ninyi nyote ni watu mnaotenda maovu!’ Mtamwona Ibrahimu, Isaka, Yakobo na manabii wote wakiwa katika ufalme wa Mungu. Lakini ninyi wenyewe mtatupwa nje. Hapo mtalia na kusaga meno yenu kwa uchungu. Watu watakuja kutoka mashariki, magharibi, kaskazini na kusini. Watakaa kuizunguka meza ya chakula katika ufalme wa Mungu. Zingatieni kwamba wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.” Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakaja kwa Yesu, na wakamwambia, “Ondoka hapa, nenda ukajifiche. Kwa sababu Herode anataka kukuua!” Lakini Yesu akawaambia, “Nendeni, mkamwambie yule mbweha, ‘Leo na kesho ninatoa pepo wachafu na kuponya watu, na kesho kazi itakwisha.’ Baada ya hilo, ni lazima niende, kwa sababu manabii wote wanapaswa kufia Yerusalemu. Yerusalemu! Yerusalemu! Uwauaye manabii. Unawapiga kwa mawe watu waliotumwa na Mungu kwako. Mara ngapi nimetaka kuwasaidia watu wako! Nilitaka kuwakusanya kama kuku anavyovikusanya vifaranga vyake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu. Mungu atakuacha ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’” Siku moja ya Sabato Yesu alikwenda nyumbani kwa miongoni mwa viongozi wa Mafarisayo kula chakula pamoja naye. Watu wote mahali pale walikuwa wanamwangalia kwa makini kuona atafanya nini. Mbele yake kulikuwa na mtu aliyekuwa na ugonjwa mbaya. Yesu akawauliza wanasheria na Mafarisayo, “Je, ni halali au kosa kuponya siku ya Sabato?” Lakini walishindwa kujibu swali lake. Hivyo akamshika yule mgonjwa, na kumponya, akamruhusu aende zake. Kisha akawaambia Mafarisayo na wanasheria, “Ikiwa mwanao au mnyama wako atatumbukia kisimani siku ya Sabato, mnatambua kuwa mtamtoa haraka.” Mafarisayo na wanasheria hawakuweza kujibu kinyume na alivyosema. Ndipo Yesu akagundua kuwa baadhi ya wageni walikuwa wanachagua sehemu za heshima za kukaa mezani. Ndipo akawaambia, “Ukialikwa na mtu katika sherehe ya harusi, usikae katika sehemu za heshima. Wanaweza kuwa wamemwalika mtu muhimu kuliko wewe. Na kama umekaa katika kiti muhimu zaidi, watakuja kwako na kukuambia ‘toka ulipokaa umpishe huyu!’ Ndipo itakulazimu kuhamia sehemu zisizo za heshima na utaaibika. Hivyo ukialikwa, nenda ukae mahali pasipo pa heshima, ili yule aliyekualika akija, akuambie, ‘Rafiki, njoo huku mbele zaidi mahali pazuri.’ Ndipo utaheshimiwa mbele ya wageni wote walio mezani pamoja nawe. Kila ajikwezaye atashushwa. Lakini ajishushaye atakwezwa.” Kisha Yesu akamwambia Farisayo aliyemwalika, “Unapoandaa chakula, usiwaalike rafiki zako tu, au ndugu zako, au jamaa zako, wala jirani zako matajiri. Kwa sababu wao pia watakualika, na kwa kufanya hivyo watakuwa wanakulipa. Lakini ufanyapo sherehe waalike maskini, waliolemaa, walemavu wa miguu, na wasiyeona. Utabarikiwa, kwa sababu watu hawa hawana kitu cha kukulipa. Lakini Mungu atakupa thawabu wakati wa ufufuo wa wenye haki.” Basi mmoja wa watu waliokuwa mezani pamoja naye aliposikia hayo akamwambia Yesu, “Wamebarikiwa watakaokula karamu katika ufalme wa Mungu.” Yesu akamwambia, “Mtu mmoja aliandaa sherehe kubwa, na kuwaalika watu wengi. Wakati wa kuanza sherehe ulipofika, alimtuma mtumishi wake awaambie wale walioalikwa, ‘Tafadhalini njooni sasa. Kila kitu kiko tayari.’ Lakini wageni waalikwa wote walisema kuwa hawawezi kuja. Kila mmoja alitoa udhuru. Wa kwanza alisema, ‘Nimenunua shamba, hivyo ni lazima niende nikalitazame. Tafadhali unisamehe.’ Mwingine alisema, ‘Nimenunua ng'ombe wa kulimia jozi tano; ni lazima niende kuwajaribu. Tafadhali unisamehe.’ Na mtu wa tatu alisema, ‘Nimeoa mke, kwa sababu hiyo siwezi kuja.’ Hivyo mtumishi alirudi na kumjulisha bwana kilichotokea. Bwana wake akakasirika, akamwambia mtumishi wake, ‘Fanya haraka! Nenda mitaani na katika vichochoro vya mji. Niletee maskini, vilema, wasiyeona na walemavu wa miguu!’ Baadaye mtumishi akamwambia, ‘Mkuu nimefanya kama ulivyoniagiza, lakini bado tuna nafasi kwa ajili ya watu wengine zaidi.’ Hivyo bwana wake akamwambia mtumishi, ‘Toka nje uende kwenye barabara zinazoelekea vijijini na kando kando ya mashamba. Waambie watu huko waje, ninataka nyumba yangu ijae! Ninakwambia, sitaki mtu hata mmoja kati ya wale niliowaalika kwanza atakayekula chakula hiki nilichoandaa.’” Watu wengi walikuwa wanasafiri pamoja na Yesu. Akawaambia, “Ikiwa unakuja kwangu na hauko tayari kuiacha familia yako, huwezi kuwa mfuasi wangu. Ukimpenda zaidi baba yako, mama yako, mke wako, watoto wako, kaka na dada zako na hata maisha yako zaidi yangu huwezi kuwa mwanafunzi wangu. Yeyote ambaye hatauchukua msalaba atakaopewa na akanifuata, hawezi kuwa mfuasi wangu. Ikiwa unataka kujenga nyumba, kwanza utakaa na kuamua ili kujua itakugharimu kiasi gani. Ni lazima uone ikiwa una pesa za kutosha kumaliza kazi ya ujenzi. Usipofanya hivyo, unaweza ukaanza kazi, lakini ukashindwa kumaliza kujenga nyumba. Na usipoweza kuimaliza, kila mtu atakucheka, Watasema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini alishindwa kumalizia.’ Ikiwa mfalme anakwenda kupigana vita na mfalme mwingine, atakaa chini kwanza na kupanga. Ikiwa ana askari elfu kumi, ataamua ikiwa ana uwezo wa kumshinda mfalme mwenye askari elfu ishirini. Akiona hawezi kumshinda mfalme mwingine, atatuma baadhi ya watu kwa mfalme mwingine ili wapatane akiwa bado yuko mbali. Ndivyo ilivyo kwa kila mmoja wenu. Lazima uache kila kitu ulichonacho. La sivyo, huwezi kuwa mfuasi wangu. Chumvi ni kitu kizuri; lakini chumvi ikipoteza ladha yake, huwezi kuitengenezea ladha tena. Haifai. Huwezi hata kuitumia kama uchafu au mbolea. Watu huitupa tu. Mnaonisikiliza, sikilizeni!” Watoza ushuru na wenye dhambi wengi waliendelea kuja kumsikiliza Yesu. Hivyo Mafarisayo na walimu wa sheria wakaanza kulalamika wakisema, “Mtazameni mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi na hata kula pamoja nao!” Hivyo Yesu akawaambia mfano huu, “Chukulia mmoja wenu ana kondoo mia, lakini mmoja akapotea. Utafanya nini? Utawaacha wale tisini na tisa na kwenda kumtafuta yule mmoja aliyepotea mpaka umpate. Na ukishampata, utafurahi sana. Utambeba mabegani mwako mpaka nyumbani. Kisha utakwenda kwa majirani na rafiki zako na utawaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimempata kondoo wangu aliyepotea!’ Katika namna hiyo hiyo ninawaambia, kunakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mtu anayeacha dhambi zake. Kuna furaha zaidi kwa ajili ya mtu mmoja anayeacha dhambi kuliko watu wema tisini na tisa ambao hudhani hawahitaji kubadilika. Fikiria kuhusu mwanamke mwenye sarafu kumi za fedha, lakini akapoteza sarafu moja kati ya hizo. Atawasha taa na kuifagia nyumba. Ataitafuta sarafu kwa bidii mpaka aione. Na akiiona, atawaita rafiki na jirani zake na kuwaaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata sarafu niliyoipoteza!’ Katika namna hiyo hiyo, ni furaha kwa malaika wa Mungu, mwenye dhambi mmoja anapotubu.” Kisha Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. Mwana mdogo alimwambia baba yake, ‘Baba, nipe sehemu ya mali ninayotarajia kurithi baadaye.’ Hivyo baba yake akagawa utajiri wake kwa wanawe wawili. Baada ya siku chache yule mdogo akauza mali zake, akachukua pesa zake na akaondoka. Akasafiri mbali katika nchi nyingine. Huko alipoteza pesa zake zote katika starehe na anasa. Baada ya kutumia vyote alivyokuwa navyo, kukatokea njaa kali katika nchi ile yote. Akawa na njaa na mhitaji wa pesa. Hivyo alikwenda kutafuta kazi kwa mwenyeji mmoja wa nchi ile, naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Alikuwa anasikia njaa kiasi kwamba alikuwa anatamani kula chakula walichokula nguruwe. Lakini hakuna mtu aliyempa chakula. Alipotambua namna alivyokuwa mjinga, akafikiri moyoni mwake na kusema, ‘Wafanyakazi wote wa baba yangu wana chakula kingi. Lakini niko hapa kama niliyekufa kwa sababu sina chakula. Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu. Nitamwambia hivi: Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe. Sistahili kuitwa mwanao tena. Lakini niruhusu niwe kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ Hivyo akaondoka na kurudi kwa baba yake. Alipokuwa mbali na nyumbani kwao, baba yake alimwona, akamwonea huruma. Akamkimbilia, akamkumbatia na kumbusu sana. Mwanaye akasema, ‘Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe; sistahili kuitwa mwanao tena.’ Lakini baba akawaambia watumishi wake, ‘Fanyeni haraka, leteni vazi maalumu, mvikeni. Pia, mvisheni viatu vizuri na pete kwenye kidole chake. Na leteni ndama aliyenona, mchinjeni ili tule na kusherehekea. Kwa sababu mwanangu alikuwa amekufa, lakini sasa yuko hai tena! Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kusherehekea. Mwanaye mkubwa alikuwa shambani. Alipoikaribia nyumba, alisikia sauti za muziki na kucheza. Akaita mmoja wa watumishi na akamwuliza, ‘Kuna nini?’ Mtumishi akasema, ‘Mdogo wako amerudi, na baba yako amechinja ndama aliyenona. Anafurahi kwa sababu amempata mwanaye akiwa salama na mzima.’ Mwana mkubwa alikasirika na hakutaka kwenda kwenye sherehe. Hivyo baba yake akatoka nje kumsihi. Lakini alimwambia baba yake, ‘Tazama, miaka yote hii nimekutumikia kama mtumishi, kamwe sijaacha kukutii! Lakini hujawahi kunipa hata mbuzi mdogo ili nisherehekee pamoja na rafiki zangu. Lakini alipokuja huyu mwanao aliyepoteza mali zako kwa makahaba, umemchinjia ndama aliyenona!’ Baba yake akamwambia, ‘Mwanangu, daima umekuwa pamoja nami, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Lakini tulipaswa kusherehekea. Mdogo wako alikuwa amekufa, lakini sasa ni hai tena. Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’” Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Alikuwepo mtu mmoja tajiri, aliyekuwa na msimamizi wa kuangalia biashara zake. Baadaye akagundua kuwa msimamizi wake alikuwa anapoteza pesa zake. Hivyo, akamwita, akamwambia, ‘Nimesikia mambo mabaya juu yako. Nipe taarifa namna ulivyosimamia pesa zangu. Huwezi kuendelea kuwa msimamizi wangu.’ Hivyo msimamizi akawaza moyoni mwaka, ‘Nitafanya nini? Bwana wangu ananiachisha kazi yangu ya usimamizi. Sina nguvu za kulima, kuomba omba naona aibu. Najua nitakalofanya! Nitafanya kitu nipate marafiki. Ili nitakapopoteza kazi yangu, watanikaribisha katika nyumba zao.’ Hivyo msimamizi akawaita mmoja mmoja wale waliokuwa wanadaiwa pesa na bwana wake. Akamwuliza wa kwanza, ‘Mkuu wangu anakudai kiasi gani?’ Akamjibu, ‘Ananidai mitungi 100 ya mafuta ya zeituni.’ Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, kaa chini, fanya haraka, badilisha iwe mitungi hamsini.’ Kisha akamwambia mwingine, ‘Na wewe kiasi gani unadaiwa?’ Akajibu, ‘Vipimo mia moja vya ngano.’ Akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, ibadilishe iwe vipimo themanini.’ Baadaye bwana wake akamsifu msimamizi asiye mwaminifu kwa sababu ya kutenda kwa busara. Ndiyo, watu wa ulimwengu huu wana busara katika kufanya biashara kati yao kuliko wana wa Mungu. Ninamaanisha hivi: Vitumieni vitu vya kidunia mlivyonavyo sasa ili muwe na ‘marafiki’ kwa ajili ya siku za baadaye. Ili wakati vitu hivyo vitakapotoweka, mtakaribishwa katika nyumba ya milele. Mtu yeyote anayeweza kuaminiwa kwa mambo madogo anaweza kuaminiwa kwa mambo makubwa pia. Mtu asiye mwaminifu katika jambo dogo hawezi kuwa mwaminifu katika jambo kubwa. Ikiwa huwezi kuaminiwa kwa mali za kidunia, huwezi kuaminiwa kwa mali za mbinguni. Na kama hauwezi kuaminiwa kwa vitu vya mtu mwingine, hautapewa vitu kwa ajili yako wewe mwenyewe. Mtumwa hawezi kuwatumikia mabwana wawili wakati mmoja, hata ninyi hamwezi. Utamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au utakuwa mwaminifu kwa mmoja na hautamjali mwingine. Pia, huwezi kumtumikia Mungu na pesa.” Mafarisayo walikuwa wakiyasikiliza mambo haya yote. Walimdhihaki Yesu kwa sababu wote walipenda pesa. Yesu aliwaambia, “Mnajifanya kuwa wenye haki mbele za watu, lakini Mungu anajua hakika kilichomo mioyoni mwenu. Jambo ambalo watu hudhani kuwa la muhimu, kwa Mungu ni chukizo. Kabla ya Yohana Mbatizaji kuja, watu walifundishwa Sheria ya Musa na maandishi ya Manabii. Lakini tangu wakati wa Yohana, Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu inahubiriwa. Na kila mtu anajitahidi sana ili kuingia katika ufalme wa Mungu. Ni rahisi sana kwa mbingu na dunia kutoweka, kuliko sehemu ndogo ya herufi katika Sheria ya Musa kutoweka. Mwanaume yeyote anayemtaliki mkewe na kumwoa mke mwingine anazini. Na mwanaume anayeoa mwanamke aliyetalikiwa anazini pia.” Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja, tajiri ambaye daima alivaa nguo za thamani sana, alikuwa tajiri sana kiasi kwamba alifurahia vitu vizuri kila siku. Alikuwepo pia maskini mmoja aliyeitwa Lazaro ambaye mwili wake ulikuwa umejaa vidonda. Mara nyingi aliwekwa kwenye lango la tajiri. Lazaro alitaka tu kula masalia ya vyakula vilivyokuwa sakafuni vilivyodondoka kutoka mezani kwa tajiri. Na mbwa walikuja na kulamba vidonda vyake. Baadaye Lazaro alikufa. Malaika walimchukua na kumweka kifuani pa Ibrahimu. Tajiri naye alikufa na kuzikwa. Alichukuliwa mpaka mahali pa mauti na akawa katika maumivu makuu. Alimwona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro akiwa kifuani pake. Akaita, ‘Baba Ibrahimu, nihurumie! Mtume Lazaro kwangu ili achovye ncha ya kidole chake kwenye maji na kuupoza ulimi wangu, kwa sababu ninateseka katika moto huu!’ Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwanangu, unakumbuka ulipokuwa unaishi? Ulikuwa na mambo yote mazuri katika maisha. Lakini Lazaro hakuwa na chochote ila matatizo. Sasa yeye anafarijiwa hapa, na wewe unateseka. Pia kuna korongo pana na lenye kina kati yetu sisi na ninyi. Hakuna anayeweza kuvuka kuja kukusaidia na hakuna anayeweza kuja huku kutoka huko.’ Tajiri akasema, ‘Basi, nakuomba baba, mtume Lazaro nyumbani kwa baba yangu duniani, Nina ndugu watano. Mtume ili akawape tahadhari wasije wakafika mahali hapa pa mateso.’ Lakini Ibrahimu akasema, ‘Wanayo Sheria ya Musa na maandishi ya manabii kwa ajili ya kuyasoma; wasikilize na kutii.’ Tajiri akasema, ‘Hapana Baba Ibrahimu! Lakini ikiwa mtu kutoka kwa wafu akiwaendea ndipo wataamua kutubu na kubadili maisha yao.’ Lakini Ibrahimu akamwambia, ‘Ikiwa ndugu zako hawatawasikiliza Musa na manabii, hawataweza kumsikiliza mtu yeyote kutoka kwa wafu.’” Yesu akawaambia wafuasi wake, “Mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi yatatokea hakika. Lakini ole wake mtu anayesababisha hili litokee. Ingekuwa vizuri kwa mtu huyo kama jiwe la kusagia lingefungwa shingoni mwake, na akatupwa baharini, kuliko kusababisha mmojawapo wa wanyenyekevu hawa kutenda dhambi. Hivyo iweni waangalifu! Ikiwa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akikukosea, umwonye. Akitubu, msamehe. Hata kama akikukosea mara saba katika siku moja, lakini akakuomba msamaha kila anapokukosea, msamehe.” Kisha mitume wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.” Bwana akasema, “Imani yenu ingekuwa kubwa kama mbegu ya haradali, mngeuambia mforosadi huu, ‘Ng'oka, ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii. Chukulia mmoja wenu ana mtumishi ambaye amekuwa shambani akilima au akichunga kondoo shambani. Akirudi kutoka shambani au machungani, utamwambia nini? Je, utamwambia, ‘Njoo ndani, keti, ule chakula’? Hapana! Utamwambia mtumishi wako, ‘Nitayarishie chakula nile. Jitayarishe na unihudumie. Nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo utakula.’ Mtumishi asipewe shukrani maalumu kwa kufanya kazi yake. Anafanya kile alichoagizwa na mkuu wake. Vivyo hivyo nanyi. Mkimaliza kufanya yote mliyoamriwa kufanya, mseme, ‘Sisi ni watumwa, hatustahili shukrani yoyote maalumu. Tumefanya kazi tunayotakiwa kufanya.’” Yesu alikuwa anasafiri kwenda Yerusalemu. Alipotoka Galilaya alisafiri akipita kando ya mpaka wa Samaria. Aliingia katika mji mdogo, na wanaume kumi walimwendea. Hawakumkaribia, kwa sababu wote walikuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Lakini watu wale wakaita kwa kupaza sauti wakisema, “Yesu! Mkuu! Tafadhali utusaidie!” Yesu alipowaona, akasema, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.” Wale watu kumi walipokuwa wanakwenda kujionesha kwa makuhani, waliponywa. Mmoja wao alipoona kuwa amepona, alirudi kwa Yesu huku akimsifu Mungu kwa kupaza sauti. Akaanguka kifudifudi miguuni pa Yesu, akamshukuru. (Alikuwa Msamaria.) Yesu akasema, “Watu kumi wameponywa, wengine tisa wako wapi? Mtu huyu wala si mmoja wa watu wetu. Ni yeye peke yake aliyerudi kumsifu Mungu?” Ndipo Yesu akamwambia, “Inuka! Unaweza kwenda. Umeponywa kwa sababu uliamini.” Baadhi ya Mafarisayo walimuuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Yesu akajibu, “Kuja kwa ufalme wa Mungu si kitu unachoweza kuona. Watu hawatasema, ‘Tazama ufalme wa Mungu uko hapa’ au ‘Ule pale!’ Hapana, Ufalme wa Mungu upo hapa pamoja nanyi.” Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Wakati utakuja, ambapo mtatamani angalau kuwa na Mwana wa Adamu hata kwa siku moja, lakini hamtaweza. Watu watawaambia, ‘Tazameni, yuko kule!’ au ‘Tazameni, yuko hapa!’ Kaeni pale mlipo; msitoke kwenda kumtafuta. Iweni na subira kwa sababu Mwana wa Adamu atakaporudi, mtatambua. Siku hiyo atang'aa kama mwanga wa radi umulikavyo angani kutoka upande mmoja hadi mwingine. Lakini kwanza, ni lazima Mwana wa Adamu ateseke kwa mambo mengi na watu wa leo watamkataa. Mwana wa Adamu atakaporudi, itakuwa kama ilivyokuwa Nuhu alipoishi. Watu walikuwa wakila, wakinywa, wakioa na kuolewa hata siku Nuhu alipoingia katika safina. Ndipo gharika ilikuja na kuwaangamiza wote. Ilikuwa vivyo hivyo katika wakati wa Lutu, Mungu alipoteketeza Sodoma. Watu wa Sodoma walikuwa wakila, wakinywa, wakinunua, wakiuza, wakipanda na kujijengea nyumba. Lakini siku ambayo Lutu alitoka Sodoma, moto na baruti vilinyesha kutoka mbinguni na kuwaua wote. Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ambayo Mwana wa Adamu atarudi. Siku hiyo, ikiwa mtu atakuwa juu ya paa ya nyumba yake, hatakuwa na muda wa kushuka kwenda ndani ya nyumba kuchukua vitu vyake. Ikiwa atakuwa shambani, hataweza kurudi nyumbani. Kumbukeni yaliyompata mke wa Lutu! Kila atakayejaribu kutunza maisha aliyonayo atayaangamiza. Lakini yeyote atakayeyasalimisha maisha yake atayaokoa. Usiku ule watu wawili wataweza kuwa wamelala katika chumba kimoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.” *** Wafuasi wake wakamuuliza, “Hii itakuwa wapi Bwana?” Yesu akajibu, “Ni kama kuutafuta mzoga, utaupata pale ambapo tai wamekusanyika.” Kisha Yesu akawafundisha wafuasi wake kwamba wanapaswa kuomba daima bila kupoteza tumaini. Akatumia simulizi hii kuwafundisha. Akasema, “Kulikuwa na mwamuzi katika mji fulani. Hakumcha Mungu wala hakujali watu walikuwa wanamfikiriaje. Na katika mji huo huo alikuwepo mwanamke mjane. Huyu alimjia mwamuzi huyu mara nyingi akimwambia, ‘Kuna mtu anayenitendea mambo mabaya. Nipe haki yangu!’ Mwanzoni mwamuzi hakutaka kumsaidia yule mwanamke. Lakini baada ya muda kupita, akawaza moyoni mwake yeye mwenyewe, ‘Simchi Mungu. Na sijali watu wananifikiriaje. Lakini mwanamke huyu ananisumbua. Nikimpa haki yake ataacha kunisumbua. Nisipomsaidia, ataendelea kunijia na anaweza kunishambulia.’” Bwana akasema, “Sikilizeni, maneno aliyosema mwamuzi mbaya yana mafundisho kwa ajili yenu. Daima Mungu atawapa mahitaji yao wateule wanaomwomba usiku na mchana. Hatachelewa kuwajibu. Ninawaambia, Mungu atawapa haki yao watu wake haraka. Lakini Mwana wa Adamu atakaporudi, atawakuta duniani watu ambao bado wanamwamini?” Walikuwepo baadhi ya watu waliojiona kuwa wenye haki na waliwadharau wengine. Yesu alitumia simulizi hii kuwafundisha: “Siku moja Farisayo na mtoza ushuru walikwenda Hekaluni kuomba. Farisayo alisimama peke yake mbali na mtoza ushuru. Farisayo aliomba akisema, ‘Ee Mungu, ninakushukuru kwa kuwa mimi si mwovu kama watu wengine. Mimi siyo kama wezi, waongo au wazinzi. Ninakushukuru kwa kuwa mimi ni bora kuliko huyu mtoza ushuru. Ninafunga mara mbili kwa wiki na kutoa sehemu ya kumi ya vyote ninavyopata!’ Mtoza ushuru alisimama peke yake pia. Lakini alipoanza kuomba, hakuthubutu hata kutazama juu mbinguni. Alijipigapiga kifua chake akijinyenyekeza mbele za Mungu. Akasema, ‘Ee Mungu, unihurumie, mimi ni mwenye dhambi.’ Ninawaambia, mtu huyu alipomaliza kuomba na kwenda nyumbani, alikuwa amepatana na Mungu. Lakini Farisayo, aliyejisikia kuwa bora kuliko wengine, hakuwa amepatana na Mungu. Watu wanaojikweza watashushwa. Lakini wale wanaojishusha watakwezwa.” Baadhi ya watu waliwaleta hata watoto wao wadogo kwa Yesu ili awawekee mikono kuwabariki. Lakini wafuasi walipoona hili, waliwakataza. Lakini Yesu aliwaalika watoto kwake na kuwaambia wafuasi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto wadogo hawa. Ukweli ni kwamba, ni lazima uupokee ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyopokea vitu, la si hivyo hautauingia.” Kiongozi wa dini akamuuliza Yesu, “Mwalimu Mwema, ni lazima nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?” Yesu akamwambia, “Kwa nini unaniita mwema? Mungu peke yake ndiye mwema. Na unazijua amri zake: ‘Usizini, usiue, usiibe, usiseme uongo, na ni lazima uwaheshimu baba na mama yako.’” Lakini yule kiongozi akasema, “Nimezitii amri zote hizi tangu nilipokuwa mdogo.” Yesu aliposikia hili, akamwambia, “Lakini kuna jambo moja unatakiwa kufanya. Uza kila kitu ulichonacho na uwape maskini pesa. Utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha, njoo unifuate.” Lakini yule mtu aliposikia Yesu anamwambia kutoa pesa zake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa sababu alikuwa tajiri sana. Yesu alipoona kuwa amehuzunika, akasema, “Itakuwa vigumu sana kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Ni rahisi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Watu waliposikia hili, wakasema, “Sasa ni nani anayeweza kuokolewa?” Yesu akajibu, “Lisilowezekana kwa wanadamu, linawezekana kwa Mungu.” Petro akasema, “Tazama! Tumeacha vyote tulivyokuwa navyo na kukufuata.” Yesu akasema, “Ninaahidi kuwa kila aliyeacha nyumba, mke, ndugu, wazazi, au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu, atapokea zaidi ya kile alichoacha. Atapokea mara nyingi zaidi katika maisha haya. Na katika ulimwengu ujao atapata mara nyingi zaidi.” Kisha Yesu alizungumza na mitume wake kumi na mbili wakiwa peke yao. Akawaaambia, “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu. Kila kitu ambacho Mungu aliwaambia manabii waandike kuhusu Mwana wa Adamu kitatokea. Atakabidhiwa kwa wasio Wayahudi, ambao watamcheka, watamtukana na kumtemea mate. Watamchapa kwa mijeledi kisha watamuua. Lakini katika siku ya tatu baada ya kifo chake, atafufuka kutoka kwa wafu.” Mitume walijaribu kulielewa hili, lakini hawakuweza; maana yake ilifichwa wasiielewe. Yesu alipofika karibu na mji wa Yeriko, mwanaume mmoja asiyeona alikuwa amekaa kando ya barabara, akiomba pesa. Aliposikia kundi la watu linapita barabarani, akauliza, “Nini kimetokea?” Walimwambia, “Yesu kutoka Nazareti anapitia hapa.” Kipofu akapasa sauti yake, akaita, “Yesu, Mwana wa Daudi, tafadhali nisaidie!” Watu waliotangulia, wakiongoza kundi, wakamkanya asiyeona, wakamwambia anyamaze. Lakini alizidi sana kupaza sauti zaidi na zaidi, “Mwana wa Daudi, tafadhali unisaidie!” Yesu alisimama pale na akasema, “Mleteni yule asiyeona kwangu!” Yule asiyeona alipofika kwa Yesu, Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Asiyeona akasema, “Bwana, nataka kuona.” Yesu akamwambia, “Unaweza kuona sasa. Umeponywa kwa sababu uliamini.” Yule mtu akaanza kuona saa ile ile. Akamfuata Yesu, akimshukuru Mungu. Kila mtu aliyeliona hili alimsifu Mungu. Yesu alikuwa anasafiri kupitia katika mji wa Yeriko. Katika mji wa Yeriko alikuwepo mtu aliyeitwa Zakayo. Alikuwa mtoza ushuru mkuu na alikuwa tajiri. Alitaka kumwona Yesu na watu wengine wengi walitaka kumwona Yesu pia. Lakini alikuwa mfupi na hakuweza kuona juu ya watu. Hivyo alikimbia akaenda mahali alipojua kuwa Yesu angepita. Kisha akapanda mkuyu ili aweze kumwona Yesu. Yesu alipofika mahali alipokuwa Zakayo, alitazama juu na kumwona akiwa kwenye mti. Yesu akasema, “Zakayo, shuka upesi! Ni lazima nikae nyumbani mwako leo.” Zakayo alishuka chini haraka. Alifurahi kuwa na Yesu nyumbani mwake. Kila mtu aliliona hili na watu wakaanza kulalamika, wakisema, “Tazama aina ya mtu ambaye Yesu anakwenda kukaa kwake. Zakayo ni mwenye dhambi!” Zakayo akamwambia Bwana, “Sikiliza Bwana nitawapa maskini nusu ya pesa zangu. Ikiwa nilimdhulumu mtu yeyote, nitamrudishia mara nne zaidi.” Yesu akasema, “Leo ni siku kwa ajili ya familia hii kuokolewa kutoka katika dhambi. Ndiyo, hata mtoza ushuru huyu ni mmoja wa wateule wa Mungu. Mwana wa Adamu alikuja kuwatafuta na kuwaokoa watu waliopotea.” Kundi la watu walipokuwa bado wanamsikiliza Yesu akizungumza mambo haya. Akaongeza kwa kuwasimulia simulizi hii. Na sasa alikuwa karibu na mji wa Yerusalemu na watu walidhani kuwa ufalme wa Mungu ulikuwa unakwenda kutokea haraka. Akasema, “Mtu mmoja maarufu alikuwa anajiandaa kwenda katika nchi ya mbali kutawazwa kuwa mfalme. Kisha arudi nyumbani na kuwatawala watu wake. Hivyo aliwaita watumishi wake kumi kwa pamoja. Akampa kila mtumishi fungu la pesa. Akamwambia kila mtumishi, ‘Zifanyie biashara pesa hizi mpaka nitakaporudi.’ Lakini watu katika ule ufalme walikuwa wanamchukia mtu huyu na hivyo walituma kundi la watu kwenda katika nchi nyingine. Walipofika huko wakasema, ‘Hatutaki mtu huyu awe mfalme wetu.’ Lakini mtu yule akatawazwa kuwa mfalme. Aliporudi nyumbani, akaagiza akasema, ‘Waiteni wale watumishi wenye pesa zangu. Ninataka kujua wamezalisha kiasi gani kutokana na pesa hizo.’ Mtumishi wa kwanza alikuja na akasema, ‘Mkuu, nilizalisha mafungu kumi ya pesa kutokana na fungu moja ulilonipa.’ Mfalme akamwambia, ‘Vizuri sana! Wewe ni mtumishi mwema. Nilikuamini kwa vitu vidogo, lakini sasa utakuwa mtawala wa miji yangu kumi.’ Mtumishi wa pili akasema, ‘Mkuu, kwa fungu moja la pesa zako, nilizalisha mafungu matano.’ Mfalme akamwambia mtumishi huyu, ‘Utatawala miji yangu mitano.’ Kisha mtumishi mwingine akaingia na akasema, ‘Mkuu, fungu lako la pesa hili hapa. Nilizifunga katika kipande cha nguo na kulificha. Niliogopa kwa sababu wewe ni mgumu. Unachukua hata pesa ambazo hukuzizalisha na kukusanya chakula ambacho hukupanda.’ Kisha mfalme akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mbaya! Nitatumia maneno yako mwenyewe kukuhukumu. Unasema kuwa mimi ni mtu mgumu, ninachukua hata pesa ambazo sikuzizalisha na nakusanya chakula ambacho sikupanda? Ikiwa hiyo ni kweli, ulipaswa kuweka pesa zangu kwa watoao riba. Ili nitakaporudi pesa hiyo iwe imezalisha faida.’ Kisha mfalme akawaambia watu waliokuwa pale, ‘Mnyang'anyeni mtumishi huyu fungu la pesa na mpeni mtumishi aliyezalisha mafungu kumi ya pesa.’ Lakini watu wakamwambia mfalme, ‘Mkuu, yule mtumishi ana mafungu kumi tayari.’ Mfalme akasema, ‘Waliozalisha faida watapata zaidi. Lakini ambao hawakuzalisha faida watanyang'anywa kila kitu. Sasa, adui zangu wako wapi? Wako wapi watu ambao hawakutaka niwe mfalme? Waleteni adui zangu hapa na waueni huku nikiangalia wanavyokufa.’” Baada ya Yesu kusema mambo haya, aliendelea kusafiri kuelekea Yerusalemu. Akakaribia Bethfage na Bethania, miji iliyo karibu na kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Kisha akawatuma wawili miongoni mwa wafuasi wake, akawaambia, “Nendeni kwenye mji mnaoweza kuuona pale. Mtakapoingia mjini, mtamwona mwanapunda amefungwa ambaye bado mtu yeyote hajampanda. Mfungueni na mleteni hapa kwangu. Kama mtu yeyote akiwauliza, ‘Kwa nini mnamfungua?’ Semeni, ‘Bwana anamhitaji.’” Wafuasi wawili wakaenda kwenye mji ule. Wakamwona punda kama Yesu alivyowaambia. Wakamfungua, lakini wamiliki wa punda wakatoka. Wakawauliza wafuasi wa Yesu, “Kwa nini mnamfungua punda wetu?” Wafuasi wakajibu, “Bwana anamhitaji.” Hivyo wafuasi wakampeleka punda kwa Yesu. Wakatandika baadhi ya nguo zao juu ya mwanapunda, kisha wakampandisha Yesu juu yake. Yesu akaanza kwenda Yerusalemu. Wafuasi walikuwa wanatandaza nguo zao njiani mbele yake. Yesu alipokaribia Yerusalemu. Alipokuwa katika njia inayotelemka kutoka kwenye Mlima wa Mizeituni, kundi lote la wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa kupaza sauti. Walimsifu Mungu kwa furaha kwa sababu ya miujiza yote waliyoiona. Walisema, “Karibu! Mungu ambariki mfalme ajaye kwa jina la Bwana! Amani iwe mbinguni, na utukufu kwa Mungu!” Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika kundi wakamwambia Yesu, “Mwalimu, waambie wafuasi wako wasiseme mambo haya!” Lakini Yesu akawajibu, “Ninawaambia ikiwa wafuasi wangu wasingesema, mawe haya yangesema kwa kupaza sauti!” Yesu alipoukaribia mji wa Yerusalemu, akautazama kisha akaanza kuulilia, akisema, “Laiti ungelijua leo kile kinachokuletea amani. Lakini kimefichwa kwako usikijue sasa. Wakati unakuja, ambao adui zako watajenga ukuta kukuzunguka na kukuzingira pande zote. Watakuteketeza wewe na watu wako wote. Hakuna jiwe hata moja katika majengo yako litaachwa juu ya jiwe jingine. Haya yote yatatokea kwa sababu hukujua wakati ambao Mungu alikuja kukuokoa.” Yesu aliingia katika eneo la Hekalu. Akaanza kuwafukuza watu waliokuwa wanauza vitu humo. Akasema, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litakuwa nyumba ya sala.’ Lakini mmeligeuza kuwa ‘maficho ya wezi.’” Yesu aliwafundisha watu kila siku katika eneo la Hekalu. Viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na baadhi ya viongozi wa watu walikuwa wakitafuta namna ya kumwua. Lakini hawakujua namna ambavyo wangefanya, kwa sababu alikuwa anazungukwa na watu kila wakati waliokuwa wakimsikiliza. Kila mtu alifurahia yale ambayo Yesu alikuwa anasema, hawakuacha kumsikiliza. Siku moja Yesu alikuwa anawafundisha watu katika eneo la Hekalu. Alikuwa anawahubiri Habari njema. Viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikwenda kuzungumza na Yesu. Wakamwambia, “Tuambie, una mamlaka gani kutenda mambo haya! Ni nani aliyekupa mamlaka hii?” Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali pia. Niambieni: Yohana alipobatiza watu, mamlaka yake ilitoka kwa Mungu au kwa watu fulani?” Makuhani, walimu wa sheria na viongozi wa Kiyahudi wakajadiliana kwa pamoja kuhusu hili. Wakasema, “Kama tukijibu ‘Ubatizo wa Yohana ulitoka kwa Mungu,’ atasema, ‘Sasa kwa nini hamkumwamini Yohana?’ Lakini kama tukisema ulitoka kwa watu fulani, watu hawa watatupiga kwa mawe mpaka tufe. Kwa sababu wote wanaamini Yohana alikuwa nabii.” Hivyo wakajibu, “Hatujui.” Ndipo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni nani alinipa mamlaka kufanya mambo haya.” Yesu akawaambia watu kisa hiki; “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Kisha akalikodisha kwa wakulima, kisha akasafiri kwa muda mrefu. Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, alimtuma mmoja wa watumishi wake kwa wakulima wale ili wampe sehemu yake ya zabibu. Lakini wakulima wale walimpiga yule mtumishi na wakamfukuza bila kumpa kitu. Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi mwingine. Wakulima walimpiga mtumishi huyu pia, wakamwaibisha na kumfukuza bila kumpa kitu. Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi wa tatu. Wakulima wakampiga sana mtumishi huyu na wakamtupa nje ya shamba la mizabibu. Mmiliki wa shamba la mizabibu akasema, ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa. Yumkini watamheshimu.’ Lakini wakulima walipomwona mwana wa mwenye shamba, wakajadiliana wakisema, ‘Huyu ni mwana wa mmiliki wa shamba. Shamba hili la mizabibu litakuwa lake. Tukimwua, litakuwa letu.’ Hivyo wakulima wakamtupa mwana wa mmiliki wa shamba nje ya shamba la mizabibu na wakamwua. Je, mmiliki wa shamba la mizabibu atafanya nini? Atakuja na atawaua wale wakulima, kisha atalikodisha shamba kwa wakulima wengine.” Watu waliposikia mfano huu, wakasema, “Hili lisije kutokea!” Lakini Yesu akawakazia macho na akasema, “Hivyo basi, Maandiko haya yanamaanisha nini: ‘Jiwe lililokataliwa na wajenzi, limekuwa jiwe kuu la pembeni?’ Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika na ikiwa jiwe hilo litaangukia, litakusaga!” Walimu wa sheria na wakuu wa makuhani waliposikia kisa hiki, walijua unawahusu wao. Hivyo walitaka kumkamata Yesu wakati huo huo, lakini waliogopa watu wangewadhuru. Hivyo viongozi wa Kiyahudi walitafuta namna ya kumtega Yesu. Walituma watu waliojifanya kuwa wenye haki, ili waweze kumnasa ikiwa angesema jambo ambalo wangeweza kutumia kinyume naye. Ikiwa angesema jambo lolote baya, wangemkamata na kumpeleka kwa gavana wa Kirumi, mwenye mamlaka ya kumhukumu na kumwadhibu. Hivyo wale watu wakamwambia Yesu, “Mwalimu, tunafahamu kwamba yale unayosema na kufundisha ni kweli. Haijalishi ni nani anasikiliza, unafundisha sawa kwa watu wote. Daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu. Tuambie, ni sahihi sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au si sahihi?” Lakini Yesu alitambua watu hawa walikuwa wanajaribu kumtega. Akawaambia, “Nionesheni sarafu ya fedha,” Kisha akauliza, “Jina na picha katika sarafu hii ni ya nani?” Wakamjibu, “Ya Kaisari.” Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari vilivyo vya Kaisari, na mpeni Mungu vilivyo vya Mungu.” Watu wale wakashangaa jibu lake la hekima. Hawakusema kitu. Hawakuweza kumtega Yesu pale mbele za watu. Hakusema chochote kibaya ambacho wangekitumia ili kumnasa. Baadhi ya Masadukayo walimwendea Yesu. (Masadukayo wanaamini watu hawatafufuka kutoka kwa wafu.) Wakamwuliza, “Mwalimu, Musa aliandika kwamba mtu aliyeoa akifa na hakuwa na watoto, kaka au mdogo wake amwoe mjane wake, ili wawe na watoto kwa ajili ya yule aliyekufa. Walikuwepo ndugu saba. Wa kwanza alioa mke lakini akafa bila ya kuwa na watoto. Wa pili akamuoa yule mwanamke kisha akafa. Na wa tatu akamwoa mwanamke na akafa. Kitu kile kile kikawatokea ndugu wote saba. Walikufa bila ya kuwa na watoto. Mwanamke akawa wa mwisho kufa. Lakini ndugu wote saba walimwoa. Sasa, watu watakapofufuka kutoka kwa wafu, atakuwa mke wa yupi?” Yesu akawaambia Masadukayo, “Watu huoana katika ulimwengu huu. Baadhi ya watu watastahili kufufuliwa kutoka kwa wafu na kuishi tena katika ulimwengu ujao. Katika maisha yale hawataoa kamwe. Katika maisha hayo, watu watakuwa kama malaika na hawatakufa. Ni watoto wa Mungu, kwa sababu wamefufuliwa kutoka kwa wafu. Musa alionesha dhahiri kwamba watu hufufuliwa kutoka kwa wafu. Alipoandika kuhusu kichaka kilichokuwa kinaungua, alisema kwamba Bwana ni ‘Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo.’ Ni Mungu wa wanaoishi tu. Hivyo watu hawa kwa hakika hawakuwa wamekufa. Ndiyo, kwa Mungu watu wote bado wako hai.” Baadhi ya walimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, jibu lako ni zuri.” Hakuna hata mmoja aliyekuwa na ujasiri wa kumwuliza swali jingine. Kisha Yesu akasema, “Kwa nini watu husema kwamba Masihi ni Mwana wa Daudi? Katika kitabu cha Zaburi, Daudi mwenyewe anasema, ‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu: Keti karibu nami upande wangu wa kulia, na nitawaweka adui zako chini ya mamlaka yako.’ Hivyo ikiwa Daudi anamwita Masihi, ‘Bwana’. Inawezekanaje Masihi awe mwana wa Daudi?” Watu wote walipokuwa wanamsikiliza Yesu, akawaambia wafuasi wake, “Iweni waangalifu dhidi ya walimu wa sheria. Wanapenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi yanayoonekana ya heshima. Na wanapenda pale watu wanapowasalimu kwa heshima maeneo ya masoko. Wanapenda kukaa sehemu za heshima katika masinagogi na sehemu za watu maarufu katika sherehe. Lakini huwalaghai wajane na kuchukua nyumba zao. Kisha kujionesha kuwa waongofu wa mioyo kuomba sala ndefu. Mungu atawaadhibu kwa hukumu kuu.” Yesu alitazama na kuwaona matajiri wakimtolea Mungu sadaka zao katika sanduku la sadaka ndani ya Hekalu. Kisha akamwona mjane maskini akiweka sarafu mbili za shaba kwenye sanduku. Akasema, “Mjane huyu maskini ametoa sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kuwa, ametoa zaidi ya hao matajiri wote. Wale wanavyo vingi, na wametoa vile ambavyo hawavihitaji. Lakini mwanamke huyu ni maskini sana, lakini ametoa vyote alivyokuwa akitegemea ili aishi.” Baadhi ya watu walikuwa wanazungumza kuhusu uzuri wa Hekalu lililojengwa kwa mawe safi na kupambwa kutokana na matoleo mbalimbali ambayo watu humtolea Mungu ili kutimiza nadhili zao. Lakini Yesu akasema, “Wakati utafika ambao yote mnayoyaona hapa yatateketezwa. Kila jiwe katika majengo haya litatupwa chini. Hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jingine.” Baadhi ya watu wakamwuliza Yesu, “Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Dalili ipi itatuonyesha kwamba ni wakati wa mambo haya kutokea?” Yesu akasema, “Iweni waangalifu, msije mkarubuniwa. Watu wengi watakuja wakitumia jina langu, watasema, ‘Mimi ndiye Masihi,’ na ‘Wakati sahihi umefika!’ Lakini msiwafuate. Mtakaposikia kuhusu vita na machafuko, msiogope. Mambo haya lazima yatokee kwanza. Lakini mwisho hautakuja haraka.” Kisha Yesu akawaambia, “Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. Kutakuwa matetemeko makubwa, kutakuwa njaa na magonjwa ya kutisha sehemu nyingi. Mambo ya kutisha yatatokea, na mambo ya kushangaza yatatokea kutoka mbinguni ili kuwaonya watu. Lakini kabla ya mambo haya yote kutokea, watu watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawahukumu katika masinagogi yao na kuwafunga gerezani. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na magavana. Watawatendea mambo haya yote kwa sababu ninyi ni wafuasi wangu. Lakini hili litawapa ninyi fursa ya kuhubiri juu yangu. Msihofu namna mtakavyojitetea, Nitawapa hekima kusema mambo ambayo adui zenu watashindwa kuyajibu. Hata wazazi wenu, ndugu zenu, jamaa, na marafiki watawageuka. Watawaua baadhi yenu. Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. Lakini hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyenu utakaopotea. Mtayaokoa maisha yenu ikiwa mtaendelea kuwa imara katika imani mnapopita katika mambo haya yote. Mtakapoona majeshi yameuzunguka mji wa Yerusalemu, ndipo mtajua kuwa wakati wa kuharibiwa kwake umefika. Watu walioko katika Uyahudi wakati huo wakimbilie milimani. Mtu yeyote atakaye kuwa Yerusalemu wakati huo aondoke haraka. Ikiwa utakuwa karibu na mji, usiingie mjini! Manabii waliandika mambo mengi kuhusu wakati ambao Mungu atawaadhibu watu wake. Wakati ninaouzungumzia ni wakati ambao mambo haya yote lazima yatokee. Wakati huu utakuwa mgumu kwa wanawake wenye mimba au wanaonyonyesha watoto wadogo, kwa sababu mambo mabaya yatakuja katika nchi hii. Mungu atawaadhibu watu wake kwa sababu wamemkasirisha. Baadhi ya watu watauawa, wengine watafanywa watumwa na kuchukuliwa katika nchi mbalimbali. Mji mtakatifu wa Yerusalemu utatekwa na kuwekwa chini ya utawala wa wageni mpaka wakati ulioruhusiwa wao kufanya hivi utakapokwisha. Mambo ya kushangaza yatatokea kwenye jua, mwezi na nyota na watu katika dunia yote wataogopa na kuchanganyikiwa kutokana na kelele za bahari na mawimbi yake. Watazimia kwa hofu na kuogopa watakapoona mambo yanayoupata ulimwengu. Kila kitu katika anga kitabadilishwa. Kisha watu watamwona Mwana wa Adamu akija katika wingu mwenye nguvu na utukufu mwingi. Mambo haya yakianza kutokea, simameni imara na msiogope. Jueni kuwa wakati wa Mungu kuwaweka huru umekaribia!” Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Tazameni miti yote. Mtini ni mfano mzuri. Unapochipua majani mnatambua kwamba majira ya joto yamekaribia. Kwa namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yanatokea, mtajua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia kuja. Ninawahakikishia kwamba, wakati mambo haya yote yatakapotokea, baadhi ya watu wanaoishi sasa watakuwa hai bado. Ulimwengu wote, dunia yote na anga vitapita, lakini maneno yangu yataishi milele. Iweni waangalifu, msiutumie muda wenu katika sherehe za ulevi na kuhangaikia maisha haya. Mkifanya hivyo, hamtaweza kufikiri vyema na mwisho unaweza kuja mkiwa hamjajiandaa. Mwisho utakuja kwa kushitukiza kwa kila mtu duniani. Hivyo, iweni tayari kila wakati. Ombeni ili muepuke mambo haya yote yatakayotokea na mweze kusimama kwa ujasiri mbele za Mwana wa Adamu.” Wakati wa mchana Yesu aliwafundisha watu katika eneo la Hekalu. Usiku alitoka nje ya mji na kukaa usiku kucha kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Kila asubuhi watu wote waliamka mapema kwenda kumsikiliza Yesu katika Hekalu. Ilikuwa karibu ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, inayoitwa Pasaka. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walitaka kumwua Yesu kwa siri kwa sababu waliogopa kile ambacho watu wangefanya. Mmoja wa mitume kumi na wawili wa Yesu aliitwa Yuda Iskariote. Shetani alimwingia Yuda, akaondoka, akaenda kuongea na viongozi wa makuhani na baadhi ya wakuu wa askari walinzi wa Hekalu. Aliongea nao kuhusu namna ya kumkabidhi Yesu kwao. Makuhani walifurahia sana hili. Wakaahidi kumlipa Yuda pesa ikiwa angefanya hivi. Akakubali, kisha alianza kusubiri muda mzuri wa kumkabidhi Yesu kwao. Alitaka kumkabidhi Yesu kwao wakati hakuna kundi la watu ambao wangeona. Siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu ilifika. Hii ni siku ambayo Wayahudi daima walichinja kondoo kwa ajili ya Pasaka. Yesu aliwaambia Petro na Yohana, “Nendeni mkaandae mlo wa Pasaka ili tule.” Wakamwambia, “Unataka tukauandae wapi?” Akawaambia, “Mtakapokuwa mnaingia mjini, mtakutana na mtu amebeba mtungi wa maji. Mfuateni. Ataingia katika nyumba. Mwambieni mmiliki wa nyumba, ‘Mwalimu anakuomba tafadhali utuoneshe chumba ambacho yeye na wafuasi wake wanaweza kulia mlo wa Pasaka.’ Mmiliki atawaonesha chumba kikubwa ghorofani kilicho tayari kwa ajili yetu. Andaeni mlo humo.” Hivyo Petro na Yohana wakaondoka. Kila kitu kilitokea kama Yesu alivyosema. Na hivyo wakauandaa mlo wa Pasaka. Wakati ulifika kwa wao kula mlo wa Pasaka. Yesu na mitume walikuwa wamekaa pamoja kuzunguka meza ya chakula. Yesu akawaambia, “Nilitaka sana kula mlo huu wa Pasaka pamoja nanyi kabla sijafa. Sitakula mlo mwingine wa Pasaka mpaka itakapopewa maana yake kamili katika ufalme wa Mungu.” Kisha Yesu akachukua kikombe kilichokuwa na divai. Akamshukuru Mungu, na akasema, “Chukueni kikombe hiki na kila mmoja anywe. Sitakunywa divai tena mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja.” Kisha akaichukua baadhi ya mkate na akamshukuru Mungu. Akaigawa vipande vipande, akawapa vipande mitume na kusema, “Mkate huu ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili yenu. Kuleni kwa kunikumbuka.” Katika namna ile ile, baada ya kula chakula, Yesu akachukua kikombe chenye divai na akasema, “Divai hii inawakilisha Agano Jipya kutoka kwa Mungu kwa watu wake. Litaanza pale damu yangu itakapomwagika kwa ajili yenu.” Yesu akasema, “Lakini hapa mezani kuna mkono wa yule atakayenisaliti kwa adui zangu. Mwana wa Adamu atakufa kama Mungu alivyoamua. Lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Adamu ili auawe.” Ndipo mitume wakaulizana, “Ni nani miongoni mwetu atafanya hivyo?” Baadaye, mitume wakaanza kubishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu. Lakini Yesu akawaambia, “Wafalme wa mataifa wanawatawala watu kama watumwa wao, na wenye mamlaka juu ya wengine wanataka kuitwa, ‘Wafadhili Wakuu’. Lakini ni lazima msiwe hivyo. Aliye na mamlaka zaidi miongoni mwenu lazima awe kama asiye na mamlaka. Anayeongoza anapaswa kuwa kama anayetumika. Nani ni mkuu zaidi: Yule anayetumika au yule aliyekaa mezani na kuhudumiwa? Kila mtu hudhani ni yule aliyekaa mezani akihudumiwa, sawa? Lakini nimekuwa pamoja nanyi kama ninayetumika. Na ninyi ndiyo mliobaki pamoja nami katika mahangaiko mengi. Hivyo ninawapa mamlaka kutawala pamoja nami katika ufalme ambao Baba yangu amenipa. Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme huo. Mtakaa katika viti vya enzi na kuwahukumu makabila kumi na mbili ya Israeli. Shetani ameomba ili awapepete kwa nguvu kama mkulima anavyopepeta ngano kwenye ungo ili mwanguke. Simoni, Simoni, nimekuombea ili usipoteze imani yako! Wasaidie ndugu zako kuwa imara utakaponirudia.” Lakini Petro akamwambia Yesu, “Bwana, niko tayari kufungwa gerezani pamoja nawe. Hata kufa pamoja nawe!” Lakini Yesu akasema, “Petro, asubuhi kabla jogoo hajawika, utakuwa umenikana mara tatu.” Kisha Yesu akawaambia mitume, “Kumbukeni nilipowatuma bila pesa, mkoba, wala viatu. Je, mlipungukiwa chochote?” Mitume wakajibu, “Hapana.” Yesu akawaambia, “Lakini sasa kama una pesa au mkoba, uchukue pamoja nawe. Kama huna upanga, uza koti lako ukanunue. Maandiko yanasema, ‘Alidhaniwa kuwa mhalifu.’ Maandiko haya lazima yatimizwe. Yaliyoandikwa kuhusu mimi yanatimilika sasa.” Wafuasi wakasema, “Tazama Bwana, hapa kuna panga mbili.” Yesu akawaambia, “Nyamazeni, acheni mazungumzo ya namna hiyo!” Yesu akaondoka mjini akaenda Mlima wa Mizeituni. Wafuasi wake wakaenda pamoja naye. (Alikuwa akienda huko mara kwa mara.) Akawaambia wafuasi wake, “Ombeni ili mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.” *** Kisha Yesu akaenda kama hatua hamsini mbali nao. Akapiga magoti na akaomba akisema, “Baba, ukiwa radhi, tafadhali usinifanye ninywe katika kikombe hiki. Lakini fanya unalotaka wewe, siyo ninalotaka mimi.” Kisha malaika kutoka mbinguni akaja akamtia nguvu. Yesu aliomba kwa nguvu zaidi na kustahimili zaidi kama mpiganaji wa mieleka akiwa katika mapambano makali. Jasho kama matone ya damu likadondoka kutoka kwenye uso wake. Alipomaliza kuomba, alikwenda kwa wafuasi wake. Akawakuta wamelala, wamechoka kwa sababu ya huzuni. Yesu akawaambia, “Kwa nini mnalala? Amkeni, ombeni mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.” Yesu alipokuwa anaongea, kundi likaja. Lilikuwa linaongozwa na Yuda, mmoja wa mitume kumi na wawili. Akamwendea Yesu ili ambusu. Lakini Yesu akamwambia, “Yuda unatumia busu la urafiki kumsaliti Mwana wa Adamu kwa adui zake?” Wafuasi wa Yesu walikuwa wamesimama pale pia. Walipoona kilichokuwa kinatokea, wakamwambia Yesu, “Bwana, tutumie panga zetu?” Na mmoja wao akautumia upanga wake. Akakata sikio la kulia la mtumishi wa kuhani mkuu. Yesu akasema, “Acha!” Kisha akaligusa sikio la mtumishi na akamponya. Yesu akaliambia lile kundi lililokuja kumkamata. Walikuwa viongozi wa makuhani, viongozi wa wazee wa Kiyahudi na askari walinzi wa Hekalu. Akawaambia, “Kwa nini mmekuja hapa mkiwa na mapanga na marungu? Mnadhani mimi ni mhalifu? Nilikuwa pamoja nanyi kila siku katika eneo la Hekalu. Kwa nini hamkujaribu kunikamata pale? Lakini sasa ni wakati wenu, wakati ambao giza linatawala.” Walimkamata Yesu na kumpeleka nyumbani kwa kuhani mkuu. Petro alimfuata Yesu lakini alikaa nyuma kwa mbali. Baadhi ya watu walikoka moto katikati ya ua kisha wakaketi pamoja. Petro naye aliketi pamoja nao. Kutokana na mwanga wa moto, mtumishi wa kike alimwona Petro amekaa pale. Akamtazama Petro usoni kwa makini. Kisha akasema, “Huyu pia alikuwa na yule mtu.” Lakini Petro akasema si kweli. Akasema, “Mwanamke, simfahamu mtu huyo!” Muda mfupi baadaye, mtu mwingine akamwona Petro na akasema, “Wewe pia ni mmoja wa lile kundi!” Lakini Petro akasema, “Wewe, mimi si mmoja wao!” Baada ya kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasema, “Ni kweli, nina uhakika mtu huyu alikuwa pamoja naye, kwa sababu yeye pia anatoka Galilaya.” Lakini Petro akasema, “Wewe, wala sijui unazungumza kuhusu nini!” Alipokuwa bado anazungumza, jogoo aliwika. Bwana aligeuka akamtazama Petro kwenye macho yake. Kisha Petro akakumbuka Bwana alivyokuwa amesema ya kwamba, “Kabla ya jogoo kuwika asubuhi, utakuwa umenikana mara tatu.” Kisha Petro akatoka nje na kulia kwa uchungu. Walinzi waliokuwa wanamlinda Yesu walimfanyia mizaha na kumpiga. Wakayafunika macho yake ili asiwaone. Kisha wakampiga na wakasema, “Tabiri, tuambie nani amekupiga!” Walimtukana pia matusi ya kila aina. Alfajiri, viongozi wazee wa watu, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikusanyika. Walimpeleka Yesu kwenye baraza lao kuu. Wakamwambia, “Tuambie ikiwa wewe ni Masihi.” Yesu akawaambia, “Hamtaniamini ikiwa nitawaambia kuwa mimi ni Masihi. Na ikiwa nitawauliza swali, hakika mtakataa kunijibu. Lakini kuanzia sasa, Mwana wa Adamu atakaa upande wa kuume wa Mungu Mwenye Nguvu.” Wote wakasema, “Kwa hiyo wewe ni Mwana wa Mungu?” Akawajibu, “Mnaweza kusema kuwa mimi ni Mwana wa Mungu.” Wakasema, “Je, tunahitaji mashahidi wengine zaidi? Sote tumesikia alichosema yeye mwenyewe!” Kisha kundi lote likasimama, wakampeleka Yesu kwa Pilato. Wakaanza kumshitaki Yesu na kumwambia Pilato, “Tumemkamata mtu huyu akijaribu kuwapotosha watu wetu. Anasema tusilipe kodi kwa Kaisari. Anajiita Masihi, mfalme.” Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ni mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Ndiyo, unaweza kusema hivyo.” Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na watu, “Sioni kosa lolote kwa mtu huyu.” Lakini waliendelea kusema, “Mafundisho yake yanasababisha matatizo katika Uyahudi yote. Alianzia Galilaya na sasa yupo hapa!” Pilato aliposikia hili, akauliza, “Mtu huyu anatoka Galilaya?” Akatambua kuwa Yesu yuko chini ya mamlaka ya Herode. Siku hizo Herode alikuwa Yerusalemu, hivyo Pilato alimpeleka Yesu kwake. Herode alipomwona Yesu alifurahi sana. Alikuwa akisikia habari zake na kwa muda mrefu alikuwa anataka kukutana na Yesu. Herode alitaka kuona muujiza, hivyo alitegemea kwamba Yesu angefanya muujiza mmoja. Akamwuliza Yesu maswali mengi, lakini Yesu hakusema chochote. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wamesimama pale wakipaza sauti zao wakimshitaki kwa Herode. Ndipo Herode na askari wake wakamcheka. Wakamfanyia mzaha kwa kumvalisha mavazi kama ambayo wafalme huvaa. Kisha Herode akamrudisha Yesu kwa Pilato. Nyakati za nyuma Pilato na Herode walikuwa maadui daima. Kuanzia siku ile wakawa marafiki. Pilato aliwaita viongozi wa makuhani, viongozi wa Kiyahudi na watu wote pamoja. Akawaambia, “Mlimleta mtu huyu kwangu. Mlisema alikuwa anawapotosha watu. Lakini nimemchunguza mbele yenu nyote na sijaona hatia juu ya kitu chochote mnachomshitakia. Hata Herode hakumwona kuwa ana hatia yo yote. Akamrudisha kwetu. Tazameni, hajafanya jambo lolote baya linalostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo, baada ya kumwadhibu kidogo nitamwacha aende zake.” *** Lakini wote walipaza sauti zao pamoja, “Mwue! Mwachie huru Baraba!” (Baraba alifungwa gerezani kwa sababu ya kuanzisha fujo mjini na kwa mauaji.) Pilato alitaka amwachie huru Yesu. Hivyo Pilato akawaambia atamwachilia. Lakini walipaza sauti tena wakisema, “Mwue, Mwue msalabani!” Mara ya tatu Pilato akawaambia watu, “Kwa nini? Amefanya kosa gani? Hana hatia. Sioni sababu ya kumwua. Hivyo nitamwachia huru baada ya kumwadhibu kidogo.” Lakini watu waliendelea kupaza sauti. Walidai Yesu auawe msalabani. Kelele zao zikawa kubwa kiasi kwamba Pilato aliamua kuwapa kile walichotaka. Walitaka Baraba aliyekuwa gerezani kwa sababu ya kuanzisha fujo na mauaji aachiwe huru. Pilato akamwachia Baraba. Na kumtoa Yesu ili auawe. Hili ndilo watu walitaka. Askari wakamwongoza Yesu kumtoa nje ya mji. Wakati huo huo mtu mmoja kutoka Kirene alikuwa anaingia mjini kutoka maeneo nje ya Yerusalemu. Askari wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu na kumfuata Yesu kwa nyuma. Kundi kubwa wakamfuata Yesu. Baadhi ya wanawake waliokuwemo kwenye kundi walilia na kuomboleza. Walimwonea huruma. Lakini Yesu aligeuka na kuwaambia, “Wanawake wa Yerusalemu, msinililie. Jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. Wakati unakuja ambapo watu watasema, ‘Wanawake wasioweza kuwa na watoto ndio ambao Mungu amewabariki. Hakika ni baraka kwamba hawana watoto wa kutunza.’ Watu wataiambia milima, ‘Tuangukieni!’ Wataviambia vilima, ‘Tufunikeni!’ Kama hili linaweza kutokea kwa mtu aliye mwema, nini kitatokea kwa wenye hatia?” Walikuwepo pia wahalifu wawili waliotolewa nje ya mji pamoja na Yesu ili wauawe. Walipelekwa mahali palipoitwa “Fuvu la Kichwa.” Askari walimpigilia Yesu msalabani pale. Waliwapigilia misalabani wahalifu pia, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine kushoto kwa Yesu. Na Yesu alikuwa anasema, “Baba uwasamehe watu hawa, kwa sababu hawajui wanalofanya.” Askari waligawana nguo zake kwa kutumia kamari. Watu walisimama pale wakiangalia kila kitu kilichokuwa kinatokea. Viongozi wa Kiyahudi walimcheka Yesu. Walisema, “Kama kweli yeye ni Masihi, Mfalme Mteule wa Mungu, basi ajiokoe. Je, hakuwaokoa wengine?” Hata askari walimcheka Yesu na kumfanyia mizaha. Walikuja na kumpa siki ya mvinyo. Wakasema, “Ikiwa wewe ni mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe!” Waliandika maneno haya kwenye kibao msalabani juu ya kichwa chake: “HUYU NI MFALME WA WAYAHUDI”. Mmoja wa wahalifu aliyekuwa ananing'inia pale akaanza kumtukana Yesu: “Wewe siye Masihi? Basi jiokoe na utuokoe sisi pia!” Lakini mhalifu mwingine alimnyamazisha asiendelee kumtukana Yesu. Akasema, “Unapaswa kumwogopa Mungu. Sisi sote tutakufa muda si mrefu. Wewe na mimi tuna hatia, tunastahili kufa kwa sababu tulitenda mabaya. Lakini mtu huyu hajafanya chochote kibaya.” Kisha akamwambia Yesu, “Unikumbuke utakapoanza kutawala kama mfalme!” Yesu akamwambia, “Ninakwambia kwa uhakika, leo utakuwa pamoja nami Paradiso.” Ilikuwa yapata saa sita mchana, lakini kulibadilika kukawa giza mpaka saa tisa alasiri, kwa sababu jua liliacha kung'aa. Pazia ndani ya Hekalu lilichanika vipande viwili. Yesu alipaza sauti akasema, “Baba, ninaiweka roho yangu mikononi mwako!” Baada ya Yesu kusema haya, akafa. Mkuu wa askari wa Kirumi aliyekuwa pale alipoona yaliyotokea, alimsifu Mungu, akisema, “Ninajua mtu huyu alikuwa mtu mwema!” Watu wengi walikuwa wametoka mjini kuja kuona tukio hili. Walipoona, wakahuzunika, wakaondoka wakiwa wanapiga vifua vyao. Watu waliokuwa marafiki wa karibu wa Yesu walikuwepo pale. Pia, walikuwepo baadhi ya wanawake waliomfuata Yesu kutoka Galilaya. Walisimama mbali kutoka msalabani, waliyaona mambo haya. Mtu mmoja aliyeitwa Yusufu kutoka mji wa Uyahudi ulioitwa Arimathaya alikuwapo pale. Alikuwa mtu mwema, aliyeishi namna Mungu alivyotaka. Alikuwa anausubiri ufalme wa Mungu uje. Yusufu alikuwa mjumbe wa baraza la Kiyahudi. Lakini hakukubali pale viongozi wengine wa Kiyahudi walipoamua kumwua Yesu. *** Alikwenda kwa Pilato na kumwomba mwili wa Yesu. Aliushusha mwili kutoka msalabani na kuufunga kwenye nguo. Kisha akauweka ndani ya kaburi lililochimbwa katika ukuta wa mwamba. Kaburi hili lilikuwa halijatumika bado. Ilikuwa jioni Siku ya Maandalizi ya Sabato. Sabato ilikuwa ianze baada ya jua kuzama. Wanawake waliotoka Galilaya pamoja na Yesu walimfuata Yusufu. Wakaliona kaburi. Ndani yake wakaona mahali alipouweka mwili wa Yesu. Kisha wakaenda kuandaa manukato yanayonukia vizuri ili kuupaka mwili wa Yesu. Siku ya Sabato walipumzika, kama ilivyoamriwa katika Sheria ya Musa. Asubuhi mapema sana siku ya Jumapili, wanawake walikwenda kaburini ulikolazwa mwili wa Yesu. Walibeba manukato yanayonukia vizuri waliyoyaandaa. Walikuta jiwe kubwa lililokuwa limeziba mlango wa kaburi limevingirishwa kutoka kwenye mlango wa kaburi. Waliingia kaburini, lakini hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. Hawakulielewa hili. Walipokuwa wangali wanashangaa, watu wawili waliovaa mavazi yaliyong'aa walisimama pembeni mwao. Wanawake waliogopa sana. Waliinama nyuso zao zikaelekea chini. Wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai hapa? Hapa ni mahali pa waliokufa. Yesu hayuko hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu. Mnakumbuka alivyosema alipokuwa Galilaya? Alisema kwamba, ‘Mwana wa Adamu lazima atatolewa kwa mamlaka ya watu wenye dhambi, lazima atauawa msalabani na kufufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu.’” Ndipo wanawake wakakumbuka Yesu alivyosema. Wanawake wakaondoka kaburini na kurudi kwa mitume kumi na mmoja na wafuasi wengine. Waliwaeleza kila kitu kilichotokea kaburini. Wanawake hawa walikuwa Mariamu Magdalena, Yoana, na Mariamu, mama yake Yakobo na wanawake wengine. Waliwaambia mitume kila kitu kilichotokea. Lakini mitume hawakuamini yale waliyosema. Ilionekana kama upuuzi. Lakini Petro alinyanyuka na kukimbia kwenda kaburini kuona. Alitazama ndani, lakini aliona nguo tu iliyotumika kuufunga mwili wa Yesu. Petro aliondoka kwenye kaburi akarudi nyumbani alikokuwa anakaa, akijiuliza nini kilichotokea. Siku hiyo hiyo, wafuasi wawili wa Yesu walikuwa wanakwenda kwenye mji mdogo uitwao Emausi, uliokuwa yapata kilomita kumi na mbili kutoka Yerusalemu. Walikuwa wanazungumza kuhusu mambo yote yaliyotokea. Walipokuwa wakizungumza, wakijadiliana juu ya mambo haya, Yesu mwenyewe aliwasogelea na akawa anatembea nao. Lakini hawakuruhusiwa kumtambua. Yesu akawauliza, “Ni mambo gani ninayosikia mnajadiliana mnapotembea?” Wale wafuasi wawili wakasimama, sura zao zilionekana zenye huzuni. Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa akasema, “Lazima wewe ni mtu pekee katika Yerusalemu ambaye hujui yaliyotokea huko.” Yesu akasema, “Unasema kuhusu nini?” Wakasema, “Ni kuhusu Yesu, kutoka Nazareti, alikuwa nabii mkuu mbele za Mungu na watu wote. Alisema na kutenda mambo makuu mengi. Lakini viongozi wetu na viongozi wa makuhani walimtoa ili ahukumiwe na kuuawa. Wakampigilia msalabani. Tulitegemea kuwa ndiye atakayeiweka huru Israeli. Lakini sasa haya yote yametokea. Na sasa kitu kingine: Imekuwa ni siku tatu tangu alipouawa, lakini leo baadhi ya wanawake kutoka kwenye kundi letu walituambia jambo la kushangaza. Mapema asubuhi hii walikwenda kaburini ambako mwili wa Yesu ulilazwa. Lakini hawakuuona mwili wake pale. Walikuja na kutuambia kuwa wamewaona malaika. Malaika waliwaambia Yesu yu hai! Hivyo baadhi ya watu walio katika kundi letu walikwenda kaburini pia. Ilikuwa kama wanawake walivyosema. Waliliona kaburi, lakini hawakumwona Yesu.” Ndipo Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga na wazito wa kuyakubali yale waliyoandika manabii. Manabii waliandika kwamba Masihi lazima ateseke kwa mambo haya kabla hajaingia katika utukufu wa ufalme wake.” Kisha akaanza kufafanua kila kitu walichosema manabii kuhusu yeye. Alianzia katika vitabu vya Musa na kusema yale waliyosema manabii kuhusu yeye. Wakakaribia mji wa Emausi, na Yesu akafanya kama vile alikuwa anaendelea mbele. Lakini walimtaka akae, wakamsihi: “Kaa nasi. Tayari ni usiku. Mchana unakaribia kwisha.” Hivyo aliingia ndani kukaa nao. Alipokuwa mezani pamoja nao ili kula chakula cha usiku, Yesu akachukua mkate na kushukuru. Kisha akaumega na kuwapa. Baada ya kufanya hivyo, wafuasi wale wawili wakaruhusiwa kumtambua. Lakini walipojua yeye ni nani, alitoweka. Wakasemezana, “Alivyokuwa anazungumza nasi tulipokuwa barabarani, tulijisikia kama moto unawaka ndani yetu. Ilitusisimua sana alipotufafanulia maana halisi ya Maandiko!” Hivyo wafuasi wale wawili wa Bwana Yesu wakasimama na kurudi Yerusalemu haraka. Walipofika Yerusalemu waliwakuta mitume kumi na mmoja wamekusanyika pamoja na wafuasi wengine wa Bwana Yesu. Kundi likawaambia wale wafuasi wawili, “Hakika Bwana amefufuka kutoka kwa wafu! Alimtokea Simoni.” Ndipo wafuasi wawili wakaeleza kilichotokea barabarani. Wakaeleza jinsi walivyomtambua Yesu aliposhiriki mkate pamoja nao. Wakati wafuasi wawili wakiwa bado wanawaeleza mambo haya wafuasi wengine, Yesu mwenyewe akaja na kusimama katikati yao. Akawaambia, “Amani iwe kwenu.” Wafuasi walishituka na wakaogopa. Walidhani wanaona mzimu. Lakini Yesu akasema, “Kwa nini mnaogopa? Na kwa nini mnakitilia mashaka kile mnachokiona? Angalieni mikono na miguu yangu. Hakika ni mimi. Niguseni. Mtaweza kuona kuwa nina mwili wenye nyama na mifupa; mzimu hauna mwili kama huu.” Mara baada ya Yesu kusema haya, aliwaonesha mikono na miguu yake. Wafuasi walishangaa na kufurahi sana walipoona kuwa Yesu alikuwa hai. Kwa kuwa bado walikuwa hawaamini wanachokiona, akawaambia, “Mna chakula chochote hapa?” Wakampa kipande cha samaki aliyepikwa. Wafuasi wake wakiwa wanaangalia akakichukua na kukila. Yesu akawaambia, “Mnakumbuka nilipokuwa pamoja nanyi? Nilisema kila kitu kilichoandikwa kuhusu mimi katika Sheria ya Musa, vitabu vya manabii na Zaburi lazima kitimilike.” Kisha Yesu akawafafanulia Maandiko ili waelewe maana yake halisi. Yesu akawaambia, “Imeandikwa kuwa Masihi atauawa na atafufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu. Mliona mambo haya yakitokea, ninyi ni mashahidi. Na maandiko yanasema inawapasa mwende na kuwahubiri watu kuwa ni lazima wabadilike na kumgeukia Mungu, ili awasamehe. Ni lazima mwanzie Yerusalemu na mhubiri ujumbe huu kwa jina langu kwa watu wa mataifa yote. *** Kumbukeni kwamba nitamtuma kwenu yule ambaye Baba yangu aliahidi. Kaeni jijini mpaka mtakapopewa nguvu hiyo kutoka mbinguni.” Yesu akawaongoza wafuasi wake kutoka nje ya Yerusalemu hadi karibu na Bethania. Akanyenyua mikono yake na kuwabariki wafuasi wake. Alipokuwa anawabariki, alitenganishwa nao na kuchukuliwa mbinguni. Wafuasi wake walimwabudu, kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha sana. Walikuwa katika Hekalu wakati wote, wakimsifu Mungu. Mwanzoni Kabla ulimwengu haujaumbwa alikuwepo Neno. Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, na Neno alikuwa Mungu. Alikuwepo pamoja na Mungu toka mwanzo. Kila kitu kilifanyika kupitia kwake. Hakuna chochote katika uumbaji wa Mungu kilichofanyika bila yeye. Ndani yake Neno kulikuwemo na uzima, na uzima huo ulikuwa nuru kwa ajili ya watu wa ulimwenguni. Nuru hiyo yamulika gizani, na giza halikuishinda. Alikuwepo mtu aliyeitwa Yohana, aliyetumwa na Mungu. Alikuja kuwaambia watu kuhusu nuru. Ili kupitia kwake watu wote waweze kusikia kuhusu yule aliye nuru na wamwamini. Yohana mwenyewe hakuwa nuru. Lakini alikuja kuwaambia watu kuhusu nuru. Nuru ya kweli, anayeleta mwangaza kwa watu wote, alikuwa tayari kuonekana kwa ulimwengu. Huyo Neno alikuwapo tayari ulimwenguni. Ulimwengu uliumbwa kupitia yeye, lakini ulimwengu haukumkubali. Alikuja kwa ulimwengu ulio wake, na watu wake mwenyewe hawakumkubali. Lakini baadhi ya watu walimkubali wakamwamini na akawapa haki ya kuwa watoto wa Mungu. Ndiyo, walikuwa watoto wa Mungu, lakini si kwa kuzaliwa kimwili. Haikuhusisha matamanio ya kibinadamu. Mungu mwenyewe aliwafanya kuwa watoto wake. Neno akafanyika kuwa mwanadamu na akaishi pamoja nasi. Tuliouna ukuu wa uungu wake; utukufu alionao Mwana pekee wa Baba. Yohana alizungumza kuhusu yeye alipopaza sauti na kusema, “Huyu ndiye niliyemzungumzia habari zake niliposema, ‘Anayekuja baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa sababu alikuwepo mwanzoni, zamani kabla sijazaliwa.’” Alikuwa amejaa neema na kweli ya Mungu, tulipokea kutoka baraka moja baada ya nyingine kutoka kwake. Hiyo ni kusema kuwa, sheria ililetwa kwetu kupitia Musa. Lakini neema na kweli imekuja kupitia Yesu Kristo. Hakuna aliyewahi kumwona Mungu isipokuwa Mwana peke yake, ambaye yeye mwenyewe ni Mungu, ametuonesha jinsi Mungu alivyo. Yuko karibu sana na Baba kiasi kwamba tunapomwona, tumemwona Mungu. Viongozi wa Kiyahudi kule Yerusalemu walituma baadhi ya makuhani na Walawi kwa Yohana kumwuliza, “Wewe ni nani?” Yohana akawaeleza kweli. Akajibu kwa wazi bila kusitasita, “Mimi siyo Masihi.” Wakamwuliza, “Sasa wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?” Yohana akawajibu, “Hapana, mimi siye Eliya.” Wakamwuliza tena, “Je, wewe ni Nabii?” Naye akawajibu, “Hapana, mimi siyo nabii.” Kisha wakamwuliza, “Wewe ni nani basi? Tueleze habari zako. Tupe jibu la kuwaambia wale waliotutuma. Unajitambulisha mwenyewe kuwa nani?” Yohana akawaambia maneno ya nabii Isaya: “‘Mimi ni mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani: Nyoosheni njia kwa ajili ya Bwana.’” Wale Wayahudi walitoka kwa Mafarisayo. Wakamwambia Yohana, “Unasema kuwa wewe siyo Masihi. Na unasema kuwa wewe siyo Eliya wala nabii. Sasa kwa nini unawabatiza watu?” Yohana akajibu, “Nawabatiza watu kwa maji. Lakini yupo mtu hapa kati yenu ambaye ninyi hamumjui. Yeye ndiye yule anayekuja baada yangu. Nami sina sifa za kuwa mtumwa anayefungua kamba za viatu vyake.” Mambo haya yote yalitokea Bethania iliyokuwa upande mwingine wa Mto Yordani. Hapa ndipo Yohana alipowabatiza watu. Siku iliyofuata Yohana akamwona Yesu akija kwake na kusema, “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu mwenye kuondoa dhambi za ulimwengu.” Huyu ndiye niliyezungumza habari zake niliposema, “Kuna mtu anayekuja baada yangu aliye mkuu zaidi yangu, kwa sababu yeye aliishi muda mrefu kabla ya kuzaliwa kwangu.” Nami sikumjua yeye ni nani. Lakini nilikuja kuwabatiza watu kwa maji ili watu wa Israeli waelewe kuwa huyo ndiye Masihi. Kisha Yohana akasema maneno yafuatayo ili kila mtu asikie, “Mimi pia sikujua nani hasa alikuwa Masihi. Lakini yule aliyenituma kubatiza aliniambia, ‘Utamwona Roho akishuka na kutua kwa mtu. Huyo ndiye atakayewabatiza watu kwa Roho Mtakatifu.’ Nami nimeyaona haya yakitokea. Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama njiwa na kutulia juu ya mtu huyu. Hivyo haya ndiyo ninayowaambia watu: ‘Yeye huyo ndiye Mwana wa Mungu.’” *** *** Siku iliyofuata Yohana alirejea tena mahali hapo pamoja na wafuasi wake wawili. Naye akamwona Yesu akitembea, hivyo akasema, “Angalieni, Mwanakondoo wa Mungu!” Wale wafuasi wake wawili walimsikia Yohana akisema haya, basi wakaondoka na kumfuata Yesu. Yesu aligeuka na kuwaona watu wawili wakimfuata. Akawauliza, “Mnataka nini?” Nao wakajibu wakimwuliza, “Rabi, unakaa wapi?” (Rabi tafsiri yake ni Mwalimu.) Yesu akajibu, “Njooni tufuatane pamoja nanyi mtapaona ninapokaa.” Hivyo wale watu wawili wakaenda pamoja naye. Wakaona mahali alipokuwa anakaa, nao wakashinda huko pamoja naye mchana wote. Hiyo ilikuwa ni saa kumi ya jioni. Watu hawa wakamfuata Yesu baada ya kusikia habari zake kutoka kwa Yohana. Mmoja wao alikuwa Andrea, nduguye Simoni Petro. Kitu cha kwanza alichokifanya Andrea kilikuwa ni kwenda kumtafuta ndugu yake Simoni. Andrea alipompata nduguye akamwambia, “Tumemwona Masihi.” (Masihi tafsiri yake ni Kristo.) Kisha Andrea akamleta Simoni nduguye kwa Yesu. Yesu akamtazama, na kumwambia, “Wewe ndiwe Simoni, mwana wa Yohana. Basi utaitwa Kefa.” (“Kefa” tafsiri yake ni “Petro”. ) Kesho yake Yesu akaamua kwenda Galilaya. Huko alikutana na Filipo na kumwambia, “Nifuate.” Filipo alikuwa mwenyeji wa mji wa Bethsaida, kama alivyokuwa Andrea na Petro. Filipo akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona mtu ambaye habari zake ziliandikwa na Musa katika sheria. Pia Manabii waliandika habari juu ya mtu huyu. Yeye ni Yesu, mwana wa Yusufu. Naye anatoka mjini Nazareti!” Lakini Nathanaeli akamwambia Filipo, “Nazareti! Je, inawezakana kupata kitu chochote chema kutoka Nazareti?” Filipo akajibu, “Njoo uone.” Yesu akamwona Nathanaeli akija kwake na papo hapo akasema, “Mtu huyu anayekuja ni Mwisraeli halisi, ambaye unayeweza kumwamini.” Nathanaeli akamwuliza Yesu, “Umenifahamu kwa namna gani?” Yesu akamjibu, “Nilikuona pale ulipokuwa chini ya mtini, kabla Filipo hajakueleza habari zangu.” Kisha Nathanaeli akasema, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Nawe ni mfalme wa Israeli.” Yesu akamwambia, “Je, umeyaamini haya kwa sababu nimekwambia kuwa nilikuona chini ya mtini? Utaona mambo makubwa zaidi ya haya.” Kisha akasema, “Mniamini ninapowaambia kwamba mtaziona mbingu zimefunguka. Na mtawaona, ‘Malaika wa Mungu wakipanda juu na kushuka chini’ kwa ajili Mwana wa Adamu.” Siku tatu baadaye kulikuwa na arusi katika mji wa Kana huko Galilaya, mama yake Yesu naye pia alikuwapo. Yesu na wafuasi wake nao walialikwa. Hapo arusini divai ilipungua, mama yake Yesu akamwambia mwanaye, “Hawana divai ya kutosha.” Yesu akajibu, “Mama, kwa nini unaniambia mambo hayo? Wakati sahihi kwangu kufanya kazi haujafika bado.” Mama yake akawaambia wahudumu wa arusi, “Fanyeni lo lote lile atakalowaambia.” Mahali hapo ilikuwepo mitungi mikubwa sita iliyotengenezwa kwa mawe iliyotumiwa na Wayahudi katika desturi yao maalumu ya kunawa. Kila mtungi mmoja ulikuwa na ujazo wa lita 80 au 120. Yesu akawaambia wale wahudumu, “Ijazeni maji hiyo mitungi.” Nao wakaijaza maji mpaka juu. Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kiasi na mumpelekee mkuu wa sherehe.” Nao wakafanya kama walivyoambiwa. Mkuu wa sherehe akayaonja yale maji, ambayo tayari yamegeuka na kuwa divai. Naye hakujua wapi ilikotoka hiyo divai, bali wahudumu walioleta yale maji wao walijua. Akamwita bwana arusi na kumwambia, “Watu wanapoandaa huleta kwanza divai iliyo bora zaidi. Baadaye, wageni wanapokuwa wametosheka, huleta divai iliyo na ubora pungufu. Lakini wewe umeandaa divai bora zaidi hadi sasa.” Ishara hii ilikuwa ya kwanza aliyoifanya Yesu katika mji wa Kana ya Galilaya. Kwa hili Yesu alionesha ukuu wake wa kimungu, na wafuasi wake wakamwamini. Kisha Yesu akashuka kwenda katika mji wa Kapernaumu. Mama yake, ndugu zake, na wafuasi wake nao walienda pamoja naye. Wote wakakaa huko kwa siku chache. Kipindi hicho wakati wa kusherehekea Pasaka ya Wayahudi ulikaribia, hivyo ikampasa Yesu kwenda Yerusalemu. Katika eneo la Hekalu aliwaona watu wakiuza ng'ombe, mbuzi na njiwa. Aliwaona wengine wakikalia meza na kufanya biashara ya kubadili fedha za watu. Yesu akatengeneza kiboko kwa kutumia vipande vya kamba. Kisha akawafukuza watu wote, kondoo na ng'ombe watoke katika eneo la Hekalu. Akazipindua meza za wafanya biashara wa kubadilisha fedha na kuzitawanya fedha zao. Baada ya hapo akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, “Viondoeni humu vitu hivi! Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa kununua na kuuza!” Haya yaliwafanya wafuasi wake kukumbuka maneno yaliyoandikwa kwenye Maandiko: “Upendo wangu mkuu kwa Hekalu lako utaniangamiza.” Baadhi ya Wayahudi wakamwambia Yesu, “Tuoneshe muujiza mmoja kama ishara kutoka kwa Mungu. Thibitisha kwamba unayo haki ya kufanya mambo haya.” Yesu akajibu, “Bomoeni hekalu hili nami nitalijenga tena kwa muda wa siku tatu.” Wakajibu, “Watu walifanya kazi kwa miaka 46 kulijenga Hekalu hili! Je, ni kweli unaamini kwamba unaweza kulijenga tena kwa siku tatu?” Lakini Yesu aliposema “hekalu hili”, alikuwa anazungumzia mwili wake. Baada ya kufufuliwa kutoka katika wafu, wafuasi wake wakakumbuka kwamba alikuwa ameyasema hayo. Hivyo wakayaamini Maandiko, na pia wakayaamini yale aliyoyasema Yesu. Yesu alikuwa Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. Watu wengi wakamwamini kwa sababu waliona ishara na miujiza alioitenda. Lakini Yesu hakuwaamini wao, kwa sababu alijua jinsi watu wote wanavyofikiri. Hakuhitaji mtu yeyote amwambie jinsi mtu fulani alivyo. Kwa sababu alikwishamjua tayari. Alikuwepo mtu aliyeitwa Nikodemu, mmoja wa Mafarisayo. Yeye alikuwa kiongozi muhimu sana wa Kiyahudi. Usiku mmoja alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa kutoka kwa Mungu. Hayupo mtu yeyote anayeweza kutenda ishara na miujiza unayotenda bila msaada wa Mungu.” Yesu akajibu, “Hakika nakuambia, ni lazima kila mtu azaliwe upya. Yeyote ambaye hajazaliwa mara ya pili hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu.” Nikodemu akasema, “Yawezekanaje mtu ambaye tayari ni mzee akazaliwa tena? Je, anaweza kuingia tena katika tumbo la mama yake na kuzaliwa kwa mara ya pili?” Yesu akamjibu, “Uniamini ninapokwambia kuwa kila mtu anapaswa kuzaliwa tena kwa maji na kwa Roho. Yeyote ambaye hakuzaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Maisha pekee ambayo watu huyapata kutoka kwa wazazi wao ni ya kimwili. Lakini maisha mapya anayopewa mtu na Roho ni ya kiroho. Usishangae kwa kuwa nilikuambia, ‘Ni lazima mzaliwe upya.’ Upepo huvuma kuelekea popote unakopenda. Unausikia, lakini huwezi kujua unakotoka na unakoelekea. Hivyo ndivyo ilivyo kwa kila aliyezaliwa kwa Roho.” Nikodemu akauliza, “Je, haya yote yanawezekana namna gani?” Yesu akasema, “Wewe ni mwalimu mashuhuri wa Israeli, inakuwaje huelewi mambo haya? Ukweli ni kwamba, tunaongea yale tunayoyafahamu. Tunayasema yale tuliyoyaona. Hata hivyo ninyi hamyakubali yale tunayowaambia. Nimewaeleza juu ya mambo ya hapa duniani, lakini hamniamini. Vivyo hivyo nina uhakika hamtaniamini hata nikiwaeleza mambo ya mbinguni! Sikiliza, hakuna mtu aliyewahi kwenda kwa Mungu mbinguni isipokuwa Mwana wa Adamu. Yeye pekee ndiye aliyekuja duniani kutoka mbinguni.” Unakumbuka yule nyoka wa shaba ambaye Musa alimwinua kule jangwani? Vivyo hivyo Mwana wa Adamu anapaswa kuinuliwa juu. Kisha kila anayemwamini aweze kuupata uzima wa milele. Kweli, hivi ndivyo Mungu alivyouonyesha upendo wake mkuu kwa ulimwengu: akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu anayemwamini asiharibiwe na mauti bali aupate uzima wa milele. Mungu alimtuma Mwanawe ili kuuokoa ulimwengu. Hakumtuma kuja kuuhukumu na kuuweka hatiani, bali kuuokoa kwa njia ya mwanawe. Wote wanaomwamini Mwana wa Mungu hawahukumiwi hatia yoyote. Lakini wale wasiomwamini wamekwisha kuhukumiwa tayari, kwa sababu hawakumwamini Mwana pekee wa Mungu. Wamehukumiwa kutokana na ukweli huu: Kwamba nuru imekuja ulimwenguni, lakini watu hawakuitaka nuru. Bali walilitaka giza, kwa sababu walikuwa wanatenda mambo maovu. Kila anayetenda maovu huichukia nuru. Hawezi kuja kwenye nuru, kwa sababu nuru itayaweka wazi matendo maovu yote aliyotenda. Lakini yeyote anayeifuata njia ya kweli huja kwenye nuru. Nayo nuru itaonesha kuwa Mungu amekuwepo katika matendo yake yote. Baada ya hayo, Yesu na wafuasi wake wakaenda katika eneo la Uyahudi. Kule Yesu alikaa pamoja na wafuasi wake na kuwabatiza watu. Yohana naye alikuwa akiwabatiza watu kule Ainoni, eneo karibu na Salemu mahali palipokuwa na maji mengi. Huko ndiko watu walipoenda kubatizwa. Hii ilikuwa kabla ya Yohana kufungwa gerezani. Baadhi ya wafuasi wa Yohana walikuwa na mabishano pamoja na Myahudi mwingine juu ya utakatifu. Ndipo wakaja kwa Yohana na kusema, “Mwalimu, unamkumbuka mtu aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Mto Yordani? Yule uliyekuwa ukimwambia kila mtu juu yake.” Huyo pia anawabatiza watu na wengi wanaenda kwake. Yohana akajibu, “Mtu anaweza tu kuyapokea yale ambayo Mungu anayatoa. Ninyi wenyewe mlinisikia nikisema, ‘Mimi siye Masihi. Mimi ni mtu yule aliyetumwa na Mungu kutengeneza njia kwa ajili ya Masihi.’ Bibi arusi siku zote yupo kwa ajili ya bwana arusi. Rafiki anayemsindikiza bwana arusi yeye hungoja na kusikiliza tu na hufurahi anapomsikia bwana arusi akiongea. Hivyo ndivyo ninavyojisikia sasa. Ninayo furaha sana kwani Masihi yuko hapa. Yeye anapaswa kuwa juu zaidi yangu mimi, na mimi napaswa kuwa chini yake kabisa.” “Anayekuja kutoka juu ni mkubwa kuliko wengine wote. Anayetoka duniani ni wa dunia. Naye huzungumza mambo yaliyo ya duniani. Lakini yeye anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wengine wote. Huyo huyasema aliyoyaona na kuyasikia, lakini watu hawayapokei anayoyasema. Bali yeyote anayepokea anayoyasema basi amethibitisha kwamba Mungu husema kweli. Na kwamba Mungu alimtuma, na yeye huwaeleza watu yale yote Mungu aliyoyasema. Huyo Mungu humpa Roho kwa ujazo kamili. Baba anampenda Mwana na amempa uwezo juu ya kila kitu. Yeyote anayemwamini Mwana anao uzima wa milele. Lakini wale wasiomtii Mwana hawataupata huo uzima. Na hawataweza kuiepuka hasira ya Mungu.” Yesu akatambua ya kwamba Mafarisayo wamesikia habari kuwa alikuwa anapata wafuasi wengi kuliko Yohana na kuwabatiza. (Lakini kwa hakika, Yesu mwenyewe hakumbatiza mtu yeyote huko; bali wafuasi wake ndiyo waliowabatiza watu kwa niaba yake.) Hivyo akaondoka Uyahudi na kurudi Galilaya. Barabara ya kuelekea Galilaya ilimpitisha Yesu katikati ya nchi ya Samaria. Akiwa Samaria Yesu akafika katika mji wa Sikari, ulio karibu na shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu. Mahali hapo ndipo kilikuwapo kisima cha Yakobo. Kutokana na safari yake kuwa ndefu Yesu alichoka, hivyo akakaa chini kando ya kisima. Nayo ilikuwa saa sita adhuhuri. Baadaye mwanamke Msamaria akaja kisimani hapo kuchota maji, na Yesu akamwambia, “Tafadhali nipe maji ninywe.” Hili lilitokea wakati wafuasi wake walipokuwa mjini kununua chakula. Mwanamke yule akajibu, “Nimeshangazwa wewe kuniomba maji unywe! Wewe ni Myahudi nami ni mwanamke Msamaria!” (Wayahudi hawana uhusiano na Wasamaria. ) Yesu akajibu, “Hujui kile Mungu anachoweza kukukirimu. Na hunijui mimi ni nani, niliyekuomba maji ninywe. Kama ungejua, nawe ungekuwa umeniomba tayari, nami ningekupa maji yaletayo uzima.” Mwanamke akasema, “Bwana, utayapata wapi maji yaliyo hai? Kisima hiki kina chake ni kirefu sana, nawe huna kitu cha kuchotea. Je, wewe ni mkuu kumzidi baba yetu Yakobo? Yeye ndiye aliyetupa kisima hiki. Yeye alikunywa kutoka kisima hiki, na wanawe, na wanyama wake wote.” Yesu akajibu, “Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. Bali yeyote anayekunywa maji ninayompa mimi hatapata kiu tena. Maji ninayowapa watu yatakuwa kama chemichemi inayobubujika ndani yao. Hayo yatawaletea uzima wa milele.” Mwanamke akamwambia Yesu, “Bwana, nipe maji hayo. Kisha sitapata kiu na sitapaswa kuja tena hapa kuchota maji.” Yesu akamwambia, “Nenda kamwite mumeo kisha urudi naye hapa.” Mwanamke akajibu, “Lakini mimi sina mume.” Yesu akamwambia, “Uko sahihi kusema kuwa huna mume. Hiyo ni kwa sababu, hata kama umekuwa na waume watano, mwanaume unayeishi naye sasa sio mume wako. Huo ndiyo ukweli wenyewe.” Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona ya kuwa wewe ni nabii. Baba zetu waliabudu katika mlima huu. Lakini ninyi Wayahudi mnasema kuwa Yerusalemu ndipo mahali ambapo watu wanapaswa kuabudia.” Yesu akasema, “Mwanamke! Niamini mimi, wakati unakuja ambapo hamtakwenda Yerusalemu wala kuja kwenye mlima huu kumwabudu Baba. Ninyi Wasamaria hamwelewi mambo mengi kuhusu yule mnayemwabudu. Sisi Wayahudi tunamfahamu vizuri tunayemwabudu, kwa maana njia yake ya kuuokoa ulimwengu imepatikana kupitia Wayahudi. Lakini wakati unakuja wenye nia halisi ya kuabudu watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa hakika, wakati huo sasa umekwishafika. Na hao ndiyo watu ambao Baba anataka wamwabudu. Mungu ni roho. Hivyo wote wanaomwabudu wanapaswa kumwabudu katika roho na kweli.” Mwanamke akasema, “Naelewa kwamba Masihi anakuja.” (Ndiye anayeitwa Kristo.) “Atakapokuja, atatufafanulia kila kitu.” Kisha Yesu akasema, “Mimi ninayezungumza nawe sasa, ndiye Masihi.” Wakati huo huo wafuasi wa Yesu wakarudi toka mjini. Nao walishangaa kwa sababu walimwona Yesu akiongea na mwanamke. Lakini hakuna aliyemwuliza yule mwanamke, “Unataka nini?” Wala Yesu, “Kwa nini unaongea naye?” Yule mwanamke akauacha mtungi wake wa maji na kurudi mjini. Akawaambia watu kule, “Mwanaume mmoja amenieleza mambo yote niliyowahi kuyafanya. Njooni mkamwone. Inawezekana yeye ndiye Masihi.” Hivyo wale watu wakatoka mjini wakaenda kumwona Yesu! Wakati huyo mwanamke akiwa mjini, wafuasi wa Yesu wakamsihi Bwana wao wakamwambia, “Mwalimu, ule chakula chochote.” Lakini Yesu akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkijui.” Hapo wafuasi wake wakaulizana, “Kwani kuna mtu yeyote hapa aliyemletea chakula mapema?” Yesu akasema, “Chakula changu ni kuimaliza kazi ile ambayo aliyenituma amenipa niifanye. Mnapopanda mimea, huwa mnasema, ‘Bado miezi minne ya kusubiri kabla ya kuvuna mazao.’ Lakini mimi ninawaambia, yafumbueni macho yenu na kuyaangalia mashamba. Sasa yako tayari kuvunwa. Hata sasa, watu wanaovuna mazao wanalipwa. Wanawaleta ndani wale watakaoupata uzima wa milele. Ili kwamba watu wanaopanda waweze kufurahi wakati huu pamoja na wale wanaovuna. Ni kweli tunaposema, ‘Mtu mmoja hupanda, lakini mwingine huvuna mazao.’ Mimi niliwatuma kukusanya mazao ambayo ninyi hamkuyahangaikia. Wengine waliyahangaikia, nanyi mnapata faida kutokana na juhudi na kazi yao.” Wasamaria wengi katika mji huo wakamwamini Yesu. Wakaamini kutokana na yale ambayo walisikia yule mwanamke akiwaambia juu ya Yesu. Aliwaambia, “Yeye amenieleza mambo yote niliyowahi kuyafanya.” Wasamaria wakaenda kwa Yesu. Wakamsihi akae pamoja nao. Naye akakaa nao kwa siku mbili. Watu wengi zaidi wakamwamini Yesu kutokana na mambo aliyoyasema. Watu hao wakamwambia mwanamke, “Mwanzoni tulimwamini Yesu kutokana na jinsi ulivyotueleza. Lakini sasa tunaamini kwa sababu tumemsikia sisi wenyewe. Sasa tunajua kwamba hakika Yeye ndiye atakayeuokoa ulimwengu.” Siku mbili baadaye Yesu akaondoka na kwenda Galilaya. (Yesu alikwishasema mwanzoni kwamba nabii huwa haheshimiwi katika nchi yake.) Alipofika Galilaya, watu wa pale walimkaribisha. Hao walikuwepo kwenye sikukuu ya Pasaka kule Yerusalemu na waliona kila kitu alichofanya huko. Naye Yesu akaenda tena kutembelea Kana huko Galilaya. Kana ni mahali alikoyabadili maji kuwa divai. Mmoja wa maafisa muhimu wa mfalme alikuwa anaishi katika mji wa Kapernaumu. Mwanawe afisa huyu alikuwa mgonjwa. Afisa huyo akasikia kwamba Yesu alikuwa amekuja kutoka Uyahudi na sasa yuko Galilaya. Hivyo akamwendea Yesu na kumsihi aende Kapernaumu kumponya mwanawe, aliyekuwa mahututi sana. Yesu akamwambia, “Ninyi watu ni lazima muone ishara zenye miujiza na maajabu kabla ya kuniamini.” Afisa wa mfalme akasema, “Bwana, uje kabla mwanangu mdogo hajafa.” Yesu akajibu, “Nenda, mwanao ataishi.” Mtu huyo akayaamini maneno Yesu aliyomwambia na akaenda nyumbani. Akiwa njiani kwenda nyumbani watumishi wake wakaja na kukutana naye. Wakasema, “Mwanao ni mzima.” Mtu huyo akauliza, “Ni wakati gani mwanangu alipoanza kupata nafuu?” Wakajibu, “Ilikuwa jana saa saba mchana homa ilipomwacha.” Baba yake akatambua kuwa saa saba kamili ulikuwa ndiyo ule wakati aliposema, “Mwanao ataishi.” Hivyo afisa huyo na kila mmoja katika nyumba yake wakamwamini Yesu. Huo ulikuwa muujiza wa pili ambao Yesu aliufanya baada ya kufika kutoka Uyahudi na Galilaya. Baadaye, Yesu akaenda Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu maalumu ya Wayahudi. Huko Yerusalemu kulikuwa na bwawa lenye mabaraza matano. Kwa Kiaramu liliitwa Bethzatha. Bwawa hili lilikuwa karibu na Lango la Kondoo. Wagonjwa wengi walikuwa wamelala katika mabaraza pembeni mwa bwawa. Baadhi yao walikuwa wasiyeona, wengine walemavu wa viungo, na wengine waliopooza mwili. Nyakati zingine malaika wa Bwana alishuka bwawani na kuyatibua maji. Baada ya hapo, mtu wa kwanza aliyeingia bwawani aliponywa ugonjwa aliokuwa nao. Mmoja wa watu waliolala hapo alikuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alimwona akiwa amelala hapo na kutambua kuwa amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu sana. Hivyo akamwuliza, “Je, unataka kuwa mzima?” Yule mgonjwa akajibu, “Bwana, hakuna mtu wa kunisaidia kuingia kwenye bwawa mara maji yanapotibuliwa. Najitahidi kuwa wa kwanza kuingia majini. Lakini ninapojaribu, mtu mwingine huniwahi na kuingia majini kabla yangu.” Kisha Yesu akasema, “Simama juu! Beba kirago chako na utembee.” Mara hiyo, mtu huyo akapona. Akabeba kirago chake na kuanza kutembea. Siku yalipotokea haya yote ilikuwa ni Siku ya Sabato. Hivyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato. Kulingana na sheria yetu wewe hauruhusiwi kubeba mkeka katika siku ya Sabato!” Lakini yeye akajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Beba mkeka wako uende.’” Wakamwuliza, “Ni nani aliyekuambia kubeba mkeka wako na kutembea?” Lakini yule mtu aliyeponywa hakuwa amemfahamu ni nani. Walikuwepo watu wengi hapo, na Yesu alikwisha kuondoka. Baadaye, Yesu akamwona huyo mtu Hekaluni na akamwambia, “Tazama, umepona sasa. Kwa hivyo uache kutenda dhambi tena, la sivyo jambo baya zaidi laweza kukupata.” Kisha huyo mtu akaondoka na kurudi kwa wale Wayahudi waliomuuliza. Naye aliwaeleza kuwa Yesu ndiye aliyemponya. Yesu alikuwa anayafanya yote haya katika siku ya Sabato. Hivyo Wayahudi hao wakaanza kumsumbua asiendelee. Lakini yeye akawaambia, “Baba yangu hajawahi kuacha kufanya kazi, hivyo nami pia nafanya kazi.” Hili likawafanya waongeze juhudi ya kumwua. Wakasema, “Mwanzoni mtu huyu alikuwa anavunja sheria kuhusu siku ya Sabato. Kisha akasema kwamba Mungu ni Baba yake! Yeye anajifanya kuwa yuko sawa na Mungu.” Lakini Yesu akajibu, “Hakika nawaambieni kuwa Mwana hawezi kufanya chochote peke yake. Bali hufanya tu yale anayoona Baba yake anayafanya. Kwa maana Mwana hufanya mambo ambayo Baba huyafanya. Baba anampenda Mwana na humwonesha kila kitu anachofanya. Pia Baba atamwonesha Mwana mambo makuu ya kufanya kuliko hili. Kisha nyote mtashangazwa. Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima. Kwa njia hiyo hiyo, Mwana pia huwapa uzima wale anaowataka.” “Vile vile, Baba hamhukumu mtu. Bali amempa Mwana nguvu ya kufanya hukumu zote. Mungu alifanya hivi ili watu wote waweze kumheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Mtu yeyote asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba. Kwani Baba ndiye aliyemtuma Mwana. Kwa hakika nawaambia, yeyote anayesikia ninayosema na kumwamini yule aliyenituma anao uzima wa milele. Hawa hawatahukumiwa kuwa na hatia. Kwani tayari wameshaivuka mauti na kuingia ndani ya uzima. Mniamini, wakati muhimu sana unakuja. Wakati huo tayari upo ambapo watu waliokufa wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu. Na hao watakaoisikia watafufuka na kuwa hai. Uzima huja kutoka kwa Baba mwenyewe. Na pia Baba amemruhusu Mwana kutoa uzima. Na Baba amempa Mwana mamlaka ya kuwahukumu watu wote kwa sababu yeye ndiye Mwana wa Adamu. Ninyi msishangazwe na hili. Wakati unakuja ambapo watu wote waliokufa na kuwamo makaburini mwao wataisikia sauti yake. Kisha watatoka nje ya makaburi yao. Wale waliotenda mema watafufuka na kupata uzima wa milele. Lakini wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa kwa kuwa na hatia. Siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninahukumu kama vile ninavyoagizwa. Na hukumu yangu ni halali, kwa sababu sitafuti kujifurahisha mwenyewe. Bali ninataka tu kumfurahisha yeye aliyenituma.” “Endapo nitawaeleza watu mambo yangu mwenyewe, watu hawatakuwa na uhakika kama yale ninayosema ni kweli. Lakini yupo mwingine anayewaeleza watu mambo yangu, nami nafahamu kuwa yale anayoyasema juu yangu ni kweli. Mliwatuma watu kwa Yohana, naye akawaambia yaliyo kweli. Hivyo sihitaji mtu yeyote wa kuwaeleza watu juu yangu, isipokuwa nawakumbusha ninyi yale aliyoyasema Yohana ili muweze kuokolewa. Yohana alikuwa kama taa iliyowaka na kutoa mwanga, nanyi mlipata raha mkiufurahia mwanga wake japo kwa muda. Hata hivyo uthibitisho nilionao mwenyewe juu yangu ni mkuu kuliko chochote alichokisema Yohana. Mambo ninayofanya ndiyo yanayonithibitisha. Haya ndiyo Baba aliyonipa kufanya. Nayo yanadhihirisha kuwa Baba alinituma. Na Baba aliyenituma yeye mwenyewe ametoa uthibitisho juu yangu. Lakini hamjawahi kabisa kuisikia sauti yake. Hamjawahi pia kuuona uso wake jinsi ulivyo. Mafundisho ya Baba hayakai ndani yenu, kwa sababu hamumwamini yule aliyetumwa na Baba. Mnajifunza Maandiko kwa makini. Nanyi mnafikiri kuwa yanawapa uzima wa milele. Maandiko haya haya yanaeleza habari zangu! Lakini mnakataa kuja kwangu kuupata huo uzima. Sitaki kutukuzwa nanyi ama na mwanadamu mwingine yeyote. Hata hivyo ninawajua ninyi, na ninajua kwamba hamna upendo kwa Mungu. Nimekuja kutoka kwa Baba yangu nami ni msemaji wake, lakini hamnikubali. Lakini watu wengine wakija wakijisemea mambo yao tu, mnawakubali! Ninyi mnapenda kupeana sifa kila mmoja kwa mwenzake. Lakini hamjaribu kupata sifa zinazotoka kwa Mungu wa pekee. Hivyo mtawezaje kuamini? Msifikiri kwamba mimi ndiye nitakayesimama mbele za Baba na kuwashtaki. Musa ndiye atakayewashtaki. Na ndiye mliyetegemea angeliwaokoa. Kama kwa hakika mlimwamini Musa, nami mlipaswa kuniamini, kwa sababu yeye aliandika habari juu yangu. Lakini hamuyaamini aliyoyaandika, hivyo hamuwezi kuyaamini ninayoyasema.” Baadaye, Yesu akavuka Ziwa Galilaya (ambalo pia linaitwa Ziwa Tiberia). Umati mkubwa wa watu ukamfuata kwa sababu waliona ishara za miujiza alizofanya kwa kuponya wagonjwa. Yesu akapanda mlimani na kukaa pale pamoja na wafuasi wake. Siku hizo sherehe ya Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. Yesu akainua macho yake na kuuona umati wa watu ukija kwake. Akamwambia Filipo, “Tunaweza kununua wapi mikate ya kuwatosha watu hawa wote?” Alimwuliza Filipo swali hili ili kumjaribu. Yesu alikwishajua kile alichopanga kufanya. Filipo akajibu, “Wote tunapaswa kufanya kazi kwa mwezi mmoja ili kununua mikate ya kutosha na kumpa kila mmoja aliyepo angalau kipande kidogo.” Mfuasi mwingine aliyekuwepo alikuwa Andrea, ndugu yake Simoni Petro. Andrea akasema, “Yupo hapa kijana mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wadogo wawili. Lakini hiyo haitoshi kwa umati huu wa watu.” Yesu akasema, “Mwambieni kila mtu akae chini.” Sehemu hiyo ilikuwa yenye nyasi nyingi, na wanaume wapatao 5,000 walikaa hapo. Yesu akaichukua ile mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya hiyo. Kisha akawapa watu waliokuwa wakisubiri kula. Alifanya vivyo hivyo kwa samaki. Akawapa watu kadiri walivyohitaji. Wote hao wakawa na chakula cha kutosha. Walipomaliza kula, Yesu akawaambia wafuasi wake, “Kusanyeni vipande vya samaki vilivyobaki na mikate ambayo haikuliwa. Msipoteze chochote.” Hivyo wakakusanya vipande vilivyobaki wakajaza vikapu 12 vikubwa vya mikate ya ngano iliyowabakia wale waliokula. Watu walikuwa wameanza kula wakiwa na vipande vitano tu vya mikate ya ngano. Watu waliiona ishara hii aliyoifanya Yesu na kusema, “Huyu atakuwa ndiye yule Nabii anayekuja ulimwenguni!” Yesu akajua kwamba watu walipanga kuja kumchukua na kumfanya kuwa mfalme wao baada ya kuona muujiza alioufanya. Hivyo akaondoka na kwenda milimani peke yake. Jioni ile wafuasi wake wakashuka kwenda ziwani. Ilikuwa giza sasa, wakati huo Yesu hakuwa pamoja na wafuasi wake. Wakapanda kwenye mashua na kuanza safari kuvuka ziwa kwenda Kapernaumu. Upepo ulikuwa unavuma kwa nguvu sana. Mawimbi ziwani yakawa makubwa. Wakaiendesha mashua kiasi cha kilomita tano au sita. Kisha wakamwona Yesu. Yeye alikuwa anatembea juu ya maji, akiifuata mashua. Nao wakaogopa. Lakini Yesu akawaambia, “Msiogope. Ni mimi.” Baada ya kusema hivyo, wakamkaribisha kwenye mashua. Kisha mashua ikafika ufukweni katika sehemu waliyotaka kwenda. Siku iliyofuata watu wengi walikuwa wamekaa upande mwingine wa ziwa. Nao walijua kuwa Yesu hakwenda pamoja na wafuasi wake kwenye mashua. Kwani walifahamu kuwa wafuasi wake waliondoka na mashua peke yao. Walijua pia kuwa ile ilikuwa ni mashua pekee iliyokuwepo pale. Lakini baadaye mashua zingine kutoka Tiberia zilifika na kusimama karibu na mahali walipokula chakula jana yake. Hapo ni mahali pale walipokula mikate baada ya Yesu kushukuru. Watu wakaona kuwa Yesu na wafuasi wake hawakuwa hapo. Hivyo wakaingia katika mashua zao na kuelekea Kapernaumu kumtafuta Yesu. Watu wakamwona Yesu akiwa upande mwingine wa ziwa. Wakamwuliza, “Mwalimu, ulifika huku lini?” Akawajibu, “Kwa nini mnanitafuta? Ni kwa sababu mliona ishara na miujiza iliyotendeka? Ukweli ni kwamba, mnanitafuta kwa vile mlikula ile mikate mkashiba. Lakini chakula cha kidunia kinaharibika na hakidumu. Ninyi msifanye kazi ili kupata chakula cha aina hiyo kinachoharibika. Isipokuwa fanyeni kazi ili mpate chakula kinachodumu na kinachowapa uzima wa milele. Mwana wa Adamu atawapa hicho chakula. Yeye ndiye pekee aliyethibitishwa na Mungu Baba kuwapa.” Watu wakamwuliza Yesu, “Mungu anatutaka tufanye nini?” Yesu akajibu, “Kazi anayoitaka Mungu muifanye ni hii: kumwamini yule aliyemtuma.” Hivyo watu wakamwuliza, “Ni ishara gani utakayotufanyia? Ili nasi tutakapokuona unafanya ishara basi tukuamini? Je, utafanya nini? Baba zetu walipewa mana kula jangwani. Kama Maandiko yanavyosema, ‘Aliwapa mkate wa kula kutoka mbinguni.’” Yesu akasema, “Naweza kuwahakikishia kwamba Musa siye aliyewapa watu wenu mkate kutoka mbinguni. Bali Baba yangu huwapa ninyi mkate halisi unaotoka mbinguni. Mkate wa Mungu ni ule unaoshuka kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.” Watu wakasema, “Bwana, kuanzia sasa na kuendelea tupe mkate wa aina hiyo.” Kisha Yesu akasema, “Mimi ndiye mkate unaoleta uzima. Hakuna ajaye kwangu atakayehisi njaa. Hakuna anayeniamini atakayepata kiu kamwe. Nilikwisha kuwaambia mapema kuwa mmeona kile ambacho naweza kufanya, lakini bado hamuniamini. Vyote anavyonipa Baba vitakuja kwangu hata hivyo yeyote Yule atakayekuja kwangu sitamkataa kabisa. Nami kwa hakika daima nitawapokea. Nilishuka kutoka mbinguni kuja kufanya yale Mungu anayopenda, siyo ninayoyapenda mimi. Nami sitampoteza hata mmoja wa wale alionipa Mungu. Bali nataka nimfufue katika siku ya mwisho. Haya ndiyo Baba yangu anayoyataka. Kila anayemtazama Mwana na kumwamini anao uzima wa milele. Nami nitamfufua katika siku ya mwisho. Hayo ndiyo anayoyataka Baba yangu.” Baadhi ya Wayahudi walianza kumlalamikia Yesu kwa vile alisema, “Mimi ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni.” Wakasema, “Huyu ni Yesu. Tunawajua baba na mama yake. Yeye ni mtoto wa Yusufu. Anawezaje kusema, ‘Nilishuka kutoka mbinguni’?” Lakini Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unika miongoni mwenu. Baba ndiye aliyenituma, na ndiye anayewaleta watu kwangu. Nami nitawafufua siku ya mwisho. Hakuna mtu anayeweza kuja kwangu asipoletwa na Baba yangu. Hii iliandikwa katika vitabu vya manabii: ‘Mungu atawafundisha wote.’ Watu humsikiliza Baba na hujifunza kutoka kwake. Hao ndiyo wanaokuja kwangu. Sina maana kwamba yupo yeyote aliyemwona Baba. Yule pekee aliyekwisha kumwona Baba ni yule aliyetoka kwa Mungu. Huyo amemwona Baba. Hakika nawaambieni kila anayeamini anao uzima wa milele. Maana mimi ni mkate unaoleta uzima. Baba zenu walikula mana waliyopewa na Mungu kule jangwani, lakini haikuwazuia kufa. Hapa upo mkate unaotoka mbinguni. Yeyote anayekula mkate huu hatakufa kamwe. Mimi ni mkate ulio hai ulioshuka kutoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu. Nitautoa mwili wangu ili watu wa ulimwengu huu waweze kupata uzima.” Kisha Wayahudi hawa wakaanza kubishana wao kwa wao. Wakasema, “Yawezekanaje mtu huyu akatupa mwili wake tuule?” Yesu akasema, “Mniamini ninaposema kwamba mnapaswa kuula mwili wa Mwana wa Adamu, na mnapaswa kuinywa damu yake. Msipofanya hivyo, hamtakuwa na uzima wa kweli. Wale wanaoula mwili wangu na kuinywa damu yangu wanao uzima wa milele. Nitawafufua siku ya mwisho. Mwili wangu ni chakula halisi, na damu yangu ni kinywaji halisi. Wale waulao mwili wangu na kuinywa damu yangu wanaishi ndani yangu, nami naishi ndani yao. Baba alinituma. Yeye anaishi, nami naishi kwa sababu yake. Hivyo kila anayenila mimi ataishi kwa sababu yangu. Mimi siyo kama ule mkate walioula baba zenu. Wao waliula mkate huo, lakini bado walikufa baadaye. Mimi ni mkate uliotoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele.” Yesu aliyasema haya yote alipokuwa akifundisha kwenye Sinagogi katika mji wa Kapernaumu. Wafuasi wa Yesu waliposikia haya, wengi wao wakasema, “Fundisho hili ni gumu sana. Nani awezaye kulipokea?” Yesu alikwishatambua kuwa wafuasi wake walikuwa wanalalamika juu ya hili. Hivyo akasema, “Je, fundisho hili ni tatizo kwenu? Ikiwa ni hivyo mtafikiri nini mtakapomwona Mwana wa Adamu akipanda kurudi kule alikotoka? Roho ndiye anayeleta uzima. Sio mwili. Lakini maneno niliyowaambia yanatoka kwa Roho, hivyo yanaleta uzima.” Lakini baadhi yenu hamuamini. (Yesu aliwafahamu wale ambao hawakuamini. Alijua haya tangu mwanzo. Na alimjua yule ambaye angemsaliti kwa adui zake.) Yesu akasema, “Ndiyo maana nilisema, ‘Hayupo hata mmoja ambaye anaweza kuja kwangu pasipo kusaidiwa na baba.’” Baada ya Yesu kusema mambo hayo, wafuasi wake wengi wakamkimbia na wakaacha kumfuata. Yesu akawauliza wale mitume kumi na wawili, “Nanyi pia mnataka kuondoka?” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutaenda wapi? Wewe unayo maneno yanayoleta uzima wa milele. Sisi tunakuamini wewe. Tunafahamu kwamba wewe ndiye Yule Mtakatifu atokaye kwa Mungu.” Kisha Yesu akajibu, “Niliwachagua nyote kumi na wawili. Lakini mmoja wenu ni Ibilisi.” Alikuwa anazungumza juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Yuda alikuwa miongoni mwa mitume kumi na wawili, lakini baadaye angemkabidhi Yesu kwa adui zake. Baada ya hayo, Yesu alitembea kuizunguka miji ya Galilaya. Hakutaka kutembelea Uyahudi, kwa sababu viongozi wa Kiyahudi kule walitaka kumuua. Huu ulikuwa ni wakati wa sherehe za sikukuu ya Wayahudi ya Vibanda. Hivyo ndugu zake wakamwambia, “Unapaswa kuondoka hapa na kwenda kwenye sikukuu Uyahudi. Kisha wafuasi wako kule wataweza kuona ishara unazofanya. Ikiwa unataka kujulikana, basi usiyafiche mambo unayoyafanya. Ikiwa unaweza kufanya mambo ya ajabu hivi, acha ulimwengu wote uone.” Ndugu zake Yesu walisema hivi kwa kuwa hata wao hawakumwamini. Yesu akawaambia, “Wakati unaonifaa kufanya hivyo haujafika, lakini kwenu ninyi kila wakati unafaa. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi. Bali ulimwengu unanichukia mimi kwa sababu nawaambia watu ulimwenguni ya kwamba wanafanya maovu. Hivyo ninyi nendeni kwenye sikukuu. Mimi sitaenda sasa, kwa sababu wakati unaonifaa haujafika.” Baada ya Yesu kusema hayo, akabaki Galilaya. Ndugu zake nao wakaondoka kwenda kwenye sikukuu ya Wayahudi ya Vibanda. Baada ya kuondoka kwao Yesu naye akaenda huko, ingawa hakutaka watu wamwone. Baada ya sikukuu ile kupita viongozi wa Kiyahudi wakawa wanamtafuta Yesu. Wakasema, “Yuko wapi huyo Yesu?” Lilikuwepo kundi la watu wengi mahali pale. Wengi kati yao walikuwa wakizungumza kwa siri kuhusu Yesu. Wengine wakasema, “Huyu ni mtu mzuri.” Lakini wengine wakakataa na kusema, “Hapana, mtu huyo huwadanganya watu.” Pamoja na hayo hakuwepo mtu aliyekuwa na busara zaidi kati yao kusema na Yesu kwa uwazi. Kwani waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Sherehe ile ilipokaribia kuisha, Yesu akaenda katika maeneo ya Hekalu na kuanza kufundisha. Viongozi wa Kiyahudi waliomsikiliza walishangazwa na kusema, “Mtu huyu amejifunza wapi mambo haya yote? Yeye hakuwahi kupata mafundisho kama yale tuliyonayo.” Yesu akajibu, “Ninayofundisha siyo yangu. Mafundisho yangu yanatoka kwake Yeye aliyenituma. Watu wanaotaka kufanya kwa uhakika kama anavyotaka Mungu watafahamu kuwa mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu. Watafahamu kwamba mafundisho haya siyo yangu. Kama ningeyafundisha mawazo yangu, ningekuwa najitafutia heshima yangu mwenyewe. Lakini kama najaribu kumletea heshima Yeye aliyenituma, basi naweza kuaminiwa. Yeyote anayefanya kama hivyo hawezi kusema uongo. Musa aliwapa sheria, sivyo? Lakini hamuitii hiyo sheria. Kama mnaitii, kwa nini basi mnataka kuniua?” Watu wakamjibu Yesu, “Pepo amekuchanganya akili! Sisi hatuna mipango ya kukuua!” Yesu akawambia, “Nilitenda ishara moja siku ya Sabato, na wote mkashangaa. Lakini mnatii sheria aliyowapa Musa kuhusu kutahiriwa; nanyi mnatahiri hata siku ya Sabato! (Lakini hakika, Musa siye aliyewatahiri. Tohara Ilitoka kwa baba zenu walioishi kabla ya Musa.) Ndiyo, siku zote mnatahiri wana wenu hata siku ya Sabato. Hii inaonesha kuwa mtu anaweza kutahiriwa siku ya Sabato ili kuitimiza sheria ya Musa. Sasa kwa nini mnanikasirikia mimi kwa kuuponya mwili wote wa mtu siku ya Sabato? Acheni kuhukumu mambo ya watu kwa jinsi mnavyoyaona. Muwe makini kutoa kuhukumu kwa njia ya haki kabisa.” Kisha baadhi ya watu waliokuwepo Yerusalemu wakasema, “Huyo ndiye mtu wanayetaka kumuua. Lakini anafundisha mahali ambapo kila mtu anaweza kumwona na kumsikia. Wala hakuna anayejaribu kumzuia kufundisha. Inawezekana viongozi wamekubali kuwa kweli yeye ni Masihi. Lakini Masihi halisi atakapokuja, hakuna atakayejua anakotoka. Nasi tunajua nyumbani kwake mtu huyu ni wapi.” Yesu alikuwa bado anafundisha katika eneo la Hekalu aliposema kwa sauti, “Ni kweli mnanijua mimi na kule ninakotoka? Niko hapa, lakini siyo kwa matakwa yangu. Nilitumwa na Yeye aliye wa kweli. Lakini ninyi hamumjui. Mimi namfahamu kwa sababu ninatoka kwake. Naye Ndiye aliyenituma.” Yesu aliposema hivi, watu wakajaribu kumkamata. Lakini hakuna aliyethubutu hata kumgusa, kwa sababu wakati unaofaa kufanya hivyo ulikuwa bado haujafika. Hata hivyo watu wengi wakamwamini Yesu. Wakasema, “Je, tunafikiri kuna haja ya kuendelea kumngojea Masihi mwingine aje atakayetenda ishara nyingine zaidi ya zile alizotenda mtu huyu?” Mafarisayo wakasikia yale ambayo watu walikuwa wakiyasema juu ya Yesu. Kwa sababu hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakawatuma walinzi wa Hekalu kwenda kumkamata. Kisha Yesu akasema, “Nitakuwa nanyi kwa muda mfupi. Kisha nitarudi kwake Yeye aliyenituma. Ninyi mtanitafuta, lakini hamtaniona. Nanyi hamwezi kuja kule nitakapokuwa.” Hawa Wayahudi wakaambiana wao kwa wao, “Huyu mtu atakwenda wapi sisi tusikoweza kufika? Je, anaweza kwenda kwenye miji ya Wayunani wanamoishi watu wetu? Je, atawafundisha Wayunani katika miji hiyo? Anasema, ‘Mtanitafuta, lakini hamtaniona.’ Vile vile anasema, ‘Hamwezi kuja kule nitakapokwenda.’ Maana yake ni nini?” Siku ya mwisho ya kusherehekea sikukuu ikafika. Nayo Ilikuwa siku muhimu zaidi. Katika siku hiyo Yesu alisimama na kusema kwa sauti kubwa, “Yeyote aliye na kiu aje kwangu anywe. Kama mtu ataniamini, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka ndani ya moyo wake. Ndivyo Maandiko yanavyosema.” Yesu alikuwa anazungumza juu ya Roho Mtakatifu ambaye alikuwa hajatolewa kwa watu bado, kwa sababu Yesu naye alikuwa bado hajatukuzwa. Ingawa baadaye, wale waliomwamini Yesu wangempokea huyo Roho. Watu waliposikia maneno aliyosema Yesu, baadhi yao wakasema, “Hakika mtu huyu ni nabii.” Wengine wakasema, “Huyu ni Masihi.” Na wengine wakasema, “Masihi hawezi kutoka Galilaya. Maandiko yanasema kwamba Masihi atatoka katika ukoo wa Daudi. Na wanasema kwamba atatoka Bethlehemu, mji alimoishi Daudi.” Kwa jinsi hiyo watu hawakukubaliana wao kwa wao kuhusu Yesu. Baadhi yao wakataka kumkamata. Lakini hakuna aliyejaribu kufanya hivyo. Walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Makuhani na Mafarisayo wakawauliza, “Kwa nini hamjamleta Yesu?” Walinzi wa Hekalu wakajibu, “Hatujawahi kumsikia mtu akisema mambo ya ajabu kiasi hicho!” Mafarisayo wakajibu, “Kwa hiyo Yesu amewadanganya hata ninyi? Hamuoni kuwa hakuna kiongozi yeyote wala sisi Mafarisayo anayemwamini? Lakini watu hao walio nje wasiojua sheria wamo katika laana ya Mungu.” Lakini Nikodemu alikuwa katika kundi lile. Naye ndiye yule aliyekwenda kumwona Yesu pale mwanzo. Naye akasema, “Sheria yetu haitaturuhusu kumhukumu mtu na kumtia hatiani kabla ya kumsikiliza kwanza na kuyaona aliyotenda?” Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Wewe nawe utakuwa umetoka Galilaya. Jifunze Maandiko. Hutapata lolote kuhusu nabii anayetoka Galilaya.” Kisha wote wakaondoka na kwenda nyumbani. Usiku ule Yesu akaenda katika mlima wa Mizeituni. Mapema asubuhi akarudi katika eneo la Hekalu. Watu wengi wakaja kwake, naye akakaa pamoja nao na kuwafundisha. Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta kwake mwanamke waliyemfumania akizini. Wakamlazimisha asimame mbele ya watu. Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, mwanamke huyu amekamatwa akifanya zinaa. Sheria ya Musa inatuagiza kumponda kwa mawe mpaka afe mwanamke wa jinsi hiyo. Je, Unasema tufanye nini?” Watu hao waliyasema haya ili kumtega Yesu. Walitaka kumkamata akisema mambo tofauti ili wapate mashtaka ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama chini na kuanza kuandika kwenye udongo kwa kidole chake. Viongozi wa Kiyahudi waliendelea kumuuliza swali lao hilo. Naye akainuka na kusema, “Yeyote hapa ambaye hajawahi kutenda dhambi awe wa kwanza kumponda jiwe mwanamke huyu.” Kisha Yesu akainama chini tena na kuendelea kuandika katika udongo. Waliposikia hayo, wale watu walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine. Wanaume wazee wakitangulia kwanza, na kisha wengine wakifuata. Wakamwacha Yesu peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake. Kisha Yesu akainua uso wake tena na kumwambia, “Wameenda wapi hao wote? Je, hakuna aliyekuhukumu kuwa una hatia?” Mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja aliyenihukumu, Bwana.” Kisha Yesu akasema, “Hata mimi sikuhukumu. Unaweza kwenda sasa, lakini usifanye dhambi tena.” Baadaye Yesu akazungumza tena na watu. Akasema, “Mimi ndiye nuru ya ulimwengu. Yeyote atakayenifuata mimi hataishi gizani kamwe. Atakuwa na nuru inayoleta uzima.” Lakini Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Unapojishuhudia mwenyewe, unakuwa ni wewe peke yako unayethibitisha kuwa mambo haya ni kweli. Hivyo hatuwezi kuyaamini unayosema.” Yesu akajibu, “Ndiyo, nasema mambo haya juu yangu mwenyewe. Lakini watu wanaweza kuamini ninayosema, kwa sababu mimi najua nilikotoka. Pia najua ninakoenda. Lakini ninyi hamjui mimi ninakotoka wala ninakoenda. Mnanihukumu kama watu wanavyowahukumu wengine. Mimi simhukumu mtu yeyote. Lakini ikiwa ninahukumu, basi hukumu yangu ni ya kweli, kwa sababu ninapohukumu sifanyi hivyo peke yangu. Baba aliyenituma yuko pamoja nami. Sheria yenu inasema kwamba mashahidi wawili wakilisema jambo hilo hilo, basi mnapaswa kukubali wanayosema. Mimi shahidi ninayeshuhudia mambo yangu mwenyewe. Na Baba yangu aliyenituma ndiye shahidi wangu mwingine.” Watu wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?” Yesu akajibu, “Hamnijui mimi wala Baba yangu hamumjui. Lakini mngenijua mimi, mngemjua Baba pia.” Yesu alisema maneno haya alipokuwa anafundisha katika eneo la Hekalu, karibu na chumba ambamo sadaka za Hekaluni zilitunzwa. Hata hivyo hakuna hata mmoja aliyemkamata, kwa sababu wakati sahihi wa kufanya hivyo ulikuwa bado haujafika. Kwa mara nyingine, Yesu akawaambia watu, “Mimi nitawaacha. Nanyi mtanitafuta, lakini pamoja na hayo mtakufa katika dhambi zenu. Kwani hamuwezi kuja kule niendako.” Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakaulizana wenyewe, “Je, atajiua mwenyewe? Je, ndiyo maana alisema, ‘Hamuwezi kuja kule niendako’?” Lakini Yesu akawaambia, “Ninyi watu ni wa hapa chini, lakini mimi ni wa kule juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu, lakini mimi si wa ulimwengu huu. Niliwaambia kwamba mnaweza kufa katika dhambi zenu. Ndiyo, kama hamtaamini kuwa MIMI NDIYE, mtakufa katika dhambi zenu.” Wakamwuliza, “Sasa wewe ni nani?” Yesu akajibu, “Mimi ni yule niliyekwisha kuwaambia tangu mwanzo kuwa ni nani. Ninayo mengi zaidi ya kusema na ya kuwahukumu. Lakini nawaambia watu yale tu niliyosikia kutoka kwake aliyenituma, naye daima husema kweli.” Wale watu hawakuelewa alikuwa anazungumza habari za nani. Kwani Yeye alikuwa anawaambia habari za Baba. Naye akawaambia, “Mtamwinua juu Mwana wa Adamu. Ndipo mtakapojua kuwa MIMI NDIYE. Mtajua kuwa lo lote nilifanyalo silifanyi kwa mamlaka yangu. Mtajua kuwa nayasema tu yale Baba yangu aliyonifundisha. Yeye aliyenituma yuko pamoja nami. Siku zote nafanya yale yanayompendeza. Naye hajawahi kuniacha peke yangu.” Yesu alipokuwa akisema mambo haya, watu wengi wakamwamini. Hivyo Yesu akawaambia Wayahudi waliomwamini, “Kama mtaendelea kuyakubali na kuyatii mafundisho yangu, mtakuwa wafuasi wangu wa kweli. Mtaijua kweli, na kweli hiyo itawafanya muwe huru.” Wakamjibu, “Sisi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Na hatujawahi kamwe kuwa watumwa. Sasa kwa nini unasema kuwa tutapata uhuru?” Yesu akasema, “Ukweli ni huu, kila anayefanya dhambi ni mtumwa wa dhambi. Mtumwa hakai na jamaa yake siku zote. Lakini mwana hukaa na jamaa yake siku zote. Hivyo kama Mwana atawapa uhuru, mtakuwa mmepata uhuru wa kweli. Najua kuwa ninyi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Lakini mmekusudia kuniua, kwa sababu hamtaki kuyakubali mafundisho yangu. Nawaambia yale ambayo Baba yangu amenionyesha. Lakini ninyi mnayafanya yale mliyoambiwa na baba yenu.” Wakasema, “Baba yetu ni Ibrahimu.” Yesu akasema, “Kama mngekuwa wazaliwa wa Ibrahimu kweli, mngefanya yale aliyofanya Ibrahimu. Mimi ni mtu niliyewaambia ukweli niliousikia kutoka kwa Mungu. Lakini Ibrahimu hakufanya kama hayo mnayotaka kufanya. Mnafanya yale aliyofanya baba yenu.” Lakini wakasema, “Sisi sio kama watoto ambao hawajawahi kumjua baba yao ni nani. Mungu ni Baba yetu. Ni baba pekee tuliye naye.” Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu kweli, mngenipenda. Nilitoka kwa Mungu, na sasa niko hapa. Sikujileta kwa mamlaka yangu mwenyewe. Mungu alinituma. Hamuyaelewi mambo ninayosema, kwa sababu hamuwezi kuyakubali mafundisho yangu. Baba yenu ni ibilisi. Ninyi ni wa kwake. Nanyi mnataka kufanya anayotaka. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo. Siku zote alikuwa kinyume na ukweli. Hakuna ukweli ndani yake. Yuko kama uongo anaousema. Ndiyo, ibilisi ni mwongo. Na ni baba wa uongo. Nawaambieni ukweli, na ndiyo maana hamniamini. Kuna mtu miongoni mwenu anayeweza kunishuhudia kuwa mimi nina hatia ya dhambi? Kama nawaeleza ukweli, kwa nini hamniamini? Yeyote aliye wa Mungu huyapokea anayosema. Lakini ninyi hamuyapokei anayosema Mungu, kwa sababu ninyi si wa Mungu.” Wayahudi wakajibu, “Sisi tunasema kuwa wewe ni Msamaria na pepo anakufanya uwe mwendawazimu! Je, hatuko sahihi kusema hivyo?” Yesu akajibu, “Sina pepo ndani yangu. Nampa heshima Baba yangu, lakini ninyi hamnipi heshima. Sijaribu kujitukuza mimi mwenyewe. Yupo mmoja anayetaka kunitukuza. Ndiye hakimu. Nawaahidi, yeyote anayeendelea kutii mafundisho yangu, hatakufa milele.” Wayahudi wakamwambia Yesu, “Sasa tunatambua kuwa una pepo ndani yako! Hata Ibrahimu na manabii walikufa. Lakini unasema, ‘Yeyote anayetii mafundisho yangu, hatakufa kamwe.’ Wewe si mkuu zaidi ya baba yetu Ibrahimu! Yeye alikufa na manabii nao walikufa. Unadhani wewe ni nani?” Yesu akajibu, “Kama ningejipa heshima mwenyewe, heshima hiyo isingelifaa kwa namna yoyote ile. Yule anayenipa mimi heshima ni Baba yangu. Ninyi mnasema kuwa ndiye Mungu wenu. Lakini kwa hakika hamumjui yeye. Mimi namjua. Kama ningesema simjui, basi ningekuwa mwongo kama ninyi. Lakini namjua, na kuyatii anayosema. Baba yenu Ibrahimu alifurahi sana kwamba angeiona siku nilipokuja duniani. Hakika aliiona na akafurahi sana.” Wayahudi wakamwambia Yesu, “Ati nini? Wawezaje kusema ulimwona Ibrahimu? Wewe bado hujafikisha hata umri wa miaka hamsini!” Yesu akajibu, “Ukweli ni kwamba, kabla Ibrahimu hajazaliwa MIMI NIPO.” Aliposema haya, wakachukua mawe ili wamponde. Lakini Yesu akajificha, na kisha akaondoka katika eneo la Hekalu. Yesu alipokuwa anatembea, alimwona mtu asiyeona tangu alipozaliwa. Wafuasi wake wakamwuliza, “Mwalimu, kwa nini mtu huyu alizaliwa asiyeona? Dhambi ya nani ilifanya hili litokee? Ilikuwa ni dhambi yake mwenyewe au ya wazazi wake?” Yesu akajibu, “Si dhambi yoyote ya huyo mtu wala ya wazazi wake iliyosababisha awe asiyeona. Alizaliwa asiyeona ili aweze kutumiwa kuonesha mambo makuu ambayo Mungu anaweza kufanya. Kukiwa bado ni mchana, tunapaswa kuendelea kuzifanya kazi zake Yeye aliyenituma. Usiku unakuja, na hakuna mtu atakayeweza kufanya kazi wakati wa usiku. Nikiwa bado nipo ulimwenguni, mimi ndiye nuru ya ulimwengu.” Yesu aliposema haya, akatema mate chini kwenye udongo, akatengeneza tope na kumpaka yule asiyeona katika macho yake. Yesu akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu” (Siloamu maana yake ni “Aliyetumwa”.) Hivyo mtu yule akaenda katika bwawa lile, akanawa na kurudi akiwa mwenye kuona. Majirani zake na wengine waliomwona akiomba omba wakasema, “Angalieni! Hivi huyu ndiye mtu yule aliyekaa siku zote na kuomba omba?” Wengine wakasema, “Ndiyo! Yeye ndiye.” Lakini wengine wakasema, “Hapana, hawezi kuwa yeye. Huyo anafanana naye tu.” Kisha yule mtu akasema, “Mimi ndiye mtu huyo.” Wakamwuliza, “Kulitokea nini? Uliwezaje kupata kuona?” Akawajibu, “Mtu yule wanayemwita Yesu alitengeneza tope akayapaka macho yangu. Kisha akaniambia ‘Nenda kanawe kwenye bwawa la Siloamu.’ Hivyo nikaenda kule na kunawa, na ndipo nikaweza kuona.” Wakamwuliza, “Yuko wapi mtu huyo?” Akajibu, “Mimi sijui aliko.” Kisha watu wakampeleka huyo mtu kwa Mafarisayo. Siku Yesu alipotengeneza yale matope na kuyaponya macho ya mtu huyo ilikuwa ni Sabato. Hivyo Mafarisayo wakamwuliza huyo mtu, “Uliwezaje kuona?” Akawajibu, “Alipaka matope katika macho yangu. Nikaenda kunawa, na sasa naweza kuona.” Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyo mtu hatii sheria inayohusu siku ya Sabato. Kwa hiyo hatoki kwa Mungu.” Wengine wakasema, “Lakini mtu aliye mtenda dhambi hawezi kufanya ishara kama hizi?” Hivyo hawakuelewana wao kwa wao. Wakamuuliza tena huyo mtu, “Kwa vile aliponya macho yako, unasemaje juu ya mtu huyo?” Akajibu, “Yeye ni nabii.” Viongozi wa Kiyahudi walikuwa bado hawaamini kwamba haya yalimtokea mtu huyo; kwamba alikuwa haoni na sasa ameponywa. Lakini baadaye wakawaita wazazi wake. Wakawauliza, “Je, huyu ni mwana wenu? Mnasema alizaliwa akiwa haoni. Sasa amewezaje kuona?” Wazazi wake wakajibu, “Tunafahamu kwamba mtu huyu ni mwana wetu. Na tunajua kuwa alizaliwa akiwa asiyeona. Lakini hatujui kwa nini sasa anaweza kuona. Hatumjui aliyeyaponya macho yake. Muulizeni mwenyewe. Yeye ni mtu mzima anaweza kujibu mwenyewe.” Walisema hivi kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Kiyahudi. Viongozi walikwisha azimia kwamba, wangemwadhibu mtu yeyote ambaye angesema Yesu alikuwa Masihi. Wangewazuia hao wasije tena kwenye sinagogi. Ndiyo maana wazazi wake walisema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni yeye!” Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakamwita yule aliyekuwa haoni. Wakamwambia aingie ndani tena. Wakasema, “Unapaswa kumheshimu Mungu na kutuambia ukweli. Tunamjua mtu huyu kuwa ni mtenda dhambi.” Yule mtu akajibu, “Mimi sielewi kama yeye ni mtenda dhambi. Lakini nafahamu hili: Nilikuwa sioni, na sasa naweza kuona!” Wakawuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyaponyaje macho yako?” Akajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia hayo. Lakini hamkutaka kunisikiliza. Kwa nini mnataka kusikia tena? Mnataka kuwa wafuasi wake pia?” Kwa hili wakampigia makelele na kumtukana wakisema, “Wewe ni mfuasi wake, siyo sisi! Sisi ni wafuasi wa Musa. Tunafahamu kwamba Mungu alisema na Musa. Lakini wala hatujui huyu mtu anatoka wapi!” Yule mtu akajibu, “Hili linashangaza kweli! Hamjui anakotoka, lakini aliyaponya macho yangu. Wote tunajua kuwa Mungu hawasikilizi watenda dhambi, bali atamsikiliza yeyote anayemwabudu na kumtii. Hii ni mara ya kwanza kuwahi kusikia kwamba mtu ameponya macho ya mtu aliyezaliwa asiyeona. Hivyo lazima anatoka kwa Mungu. Kama asingetoka kwa Mungu, asingefanya jambo lolote kama hili.” Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ulizaliwa ukiwa umejaa dhambi. Unataka kutufundisha sisi?” Kisha wakamwambia atoke ndani ya sinagogi na kukaa nje. Yesu aliposikia kuwa walimlazimisha huyo mtu kuondoka, alikutana naye na kumuuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?” Yule mtu akajibu, “Niambie ni nani huyo, bwana, ili nimwamini.” Yesu akamwambia, “Umekwisha kumwona tayari. Mwana wa Adamu ndiye anayesema nawe sasa.” Yule mtu akajibu, “Ndiyo, ninaamini, Bwana!” Kisha akainama na kumwabudu Yesu. Yesu akasema, “Nilikuja ulimwenguni ili ulimwengu uweze kuhukumiwa. Nilikuja ili wale wasiyeona waweze kuona. Kisha nilikuja ili wale wanaofikiri wanaona waweze kuwa wasiyeona.” Baadhi ya Mafarisayo walikuwa karibu na Yesu. Wakamsikia akisema haya. Wakamwuliza, “Nini? Unasema sisi pia ni wale wasiyeona?” Yesu akasema, “Kama mngekuwa wasiyeona hakika, msingekuwa na hatia ya dhambi. Lakini kwa kuwa mnasema mnaona, basi bado mngali na hatia.” Yesu akawaambia, “Hakika ninawaambia, mtu anapoingia katika zizi la kondoo, hutumia mlango. Kama akiingia kwa kutumia njia nyingine yoyote, huyo ni mwizi. Anajaribu kuwaiba kondoo. Lakini mtu anayewachunga kondoo hupitia mlangoni. Yeye ndiye mchungaji. Mtu anayelinda mlangoni humfungulia mlango mchungaji. Na kondoo huisikiliza sauti ya mchungaji wao. Naye huwaita kondoo wake mwenyewe kwa majina yao, na huwaongoza kwenda nje. Mchungaji huwatoa nje kondoo wake wote. Kisha huwatangulia mbele na kuwaongoza. Kondoo nao humfuata, kwa sababu wanaifahamu sauti yake. Lakini kamwe kondoo hawatamfuata wasiyemfahamu. Bali watamkimbia, kwa sababu hawaifahamu sauti yake.” Yesu aliwaambia watu habari hii, lakini hawakuelewa ilikuwa ina maana gani. Hivyo Yesu akasema tena, “Hakika ninawaambia, Mimi ni mlango wa kondoo. Wote walionitangulia walikuwa wezi na wanyang'anyi. Kondoo hawakuwasikiliza hao. Mimi ni mlango. Yeyote anayeingia kupitia kwangu ataokoka. Ataweza kuingia na kutoka nje. Atapata kila anachohitaji. Mwizi anakuja kuiba, kuua, na kuangamiza. Lakini mimi nilikuja kuwaletea uzima, na muwe nao kwa ukamilifu. Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo. Mtumishi anayelipwa ili kuwachunga kondoo yuko tofauti na mchungaji. Mtumishi wa mshahara, kondoo siyo mali yake. Hivyo anapomwona mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo peke yao. Mbwa mwitu huwashambulia na kuwatawanya kondoo. Mtu huyu huwakimbia kondoo kwa sababu yeye ni mfanyakazi wa mshahara tu. Hawajali kabisa kondoo. Mimi ni mchungaji ninayewajali kondoo. Nawafahamu kondoo wangu kama ambavyo Baba ananijua mimi. Na kondoo wananijua kama nami ninavyomjua Baba. Nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo hawa. *** Nina kondoo wengine ambao hawamo kwenye kundi hili hapa. Hao nao napaswa kuwaongoza. Kwani wataisikia sauti yangu. Baadaye kutakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. Baba ananipenda kwa sababu nautoa uhai wangu. Nautoa uhai wangu ili niweze kuuchukua tena. Hakuna anayeweza kuuchukua uhai wangu kutoka kwangu. Nautoa uhai wangu kwa hiari yangu. Ninayo haki ya kuutoa, na ninayo haki ya kuuchukua tena. Haya ndiyo aliyoniambia Baba yangu.” Kwa mara nyingine tena Wayahudi wakagawanyika juu ya yale aliyoyasema Yesu. Wengi wao wakasema, “Pepo mchafu amemwingia na kumfanya awe mwendawazimu. Kwa nini sisi tumsikilize?” Lakini wengine wakasema, “Haya siyo maneno ya mtu anayeendeshwa na pepo mchafu. Pepo mchafu hawezi kuponya macho ya mtu asiyeona.” Ulikuwa ni wakati wa baridi, na wakati wa Sikukuu ya Kuweka Wakfu kule Yerusalemu. Yesu alikuwa katika eneo la Hekalu katika Ukumbi wa Sulemani. Viongozi wa Kiyahudi wakakusanyika kumzunguka. Wakasema, “Ni mpaka lini utatuacha na mashaka juu yako? Kama wewe ndiwe Masihi, basi tuambie wazi wazi.” Yesu akajibu, “Nilikwisha kuwaambia tayari, lakini hamkuamini. Nafanya miujiza katika jina la Baba yangu. Miujiza hii inaonesha mimi ni nani. Lakini hamuamini, kwa sababu ninyi siyo kondoo wangu. Kondoo wangu huisikia sauti yangu. Nami nawajua, nao hunifuata. Mimi nawapa kondoo wangu uzima wa milele. Nao hawatakufa kamwe, na tena hakuna atakayemchukua yeyote kutoka mkononi mwangu. Baba yangu ndiye aliyenipa hao, naye ni mkuu kuliko wote. Hakuna anayeweza kuwaiba kondoo wangu kutoka mkononi mwangu. Mimi na Baba tu umoja.” Kwa mara nyingine Wayahudi pale wakaokota mawe ili wamuue Yesu. Lakini Yeye akawaambia, “Mambo mengi mliyoyaona nikiyatenda yanatoka kwa Baba. Ni kwa mambo gani miongoni mwa hayo mazuri mnataka kuniua?” Wakajibu, “Hatukuui kwa ajili ya jambo lo lote zuri ulilofanya. Lakini wewe unasema mambo yanayomkufuru Mungu! Wewe ni mtu tu, lakini unasema uko sawa na Mungu! Ndiyo sababu tunataka kukuua!” Yesu akajibu, “Imeandikwa katika sheria yenu kuwa Mungu alisema, ‘Nilisema ninyi ni miungu.’ Maandiko yaliwaita watu hawa miungu; watu waliopokea ujumbe wa Mungu. Na Maandiko siku zote ni ya kweli. Sasa kwa nini mnanilaumu mimi kwa kumkufuru Mungu kwa kusema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu’? Lakini kama sitafanya yale anayoyatenda Baba yangu, basi msiamini ninayosema. Lakini kama nafanya anayofanya Baba, mnapaswa kuyaamini ninayoyafanya. Mnaweza msiniamini mimi, lakini muamini yale ninayotenda. Ndipo mtakapofahamu na kuelewa kwamba Baba yumo ndani yangu nami nimo ndani ya Baba.” Walijaribu kumkamata Yesu tena, lakini yeye akawatoroka. Kisha akarejea tena kwa kuvuka Mto Yordani hadi sehemu ambapo Yohana alipoanzia kazi ya kubatizia watu. Yesu akakaa huko, na watu wengi wakaja kwake. Wakasema, “Yohana hakutenda ishara na miujiza yoyote, lakini kila alichosema kuhusu mtu huyu ni kweli!” Na watu wengi huko wakamwamini Yesu. Alikuwepo mtu aliyekuwa mgonjwa aliyeitwa Lazaro. Huyo aliishi katika mji wa Bethania, mahali ambapo Mariamu na dada yake Martha waliishi. (Mariamu ni mwanamke yule aliyempaka Bwana manukato na kumpangusa miguu kwa nywele zake.) Ndugu wa Mariamu alikuwa Lazaro, ambaye sasa alikuwa mgonjwa. Kwa hiyo Mariamu na Martha walimtuma mtu kwa Yesu kumwambia, “Bwana, rafiki yako mpendwa Lazaro ni mgonjwa.” Yesu aliposikia hayo alisema, “ugonjwa huu sio wa kifo. Isipokuwa, ugonjwa huu ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Hili limetokea ili kuleta utukufu kwa Mwana wa Mungu.” Yesu aliwapenda Martha, na dada yake na Lazaro. Hivyo aliposikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, akabaki alipokuwa kwa siku mbili zaidi, kisha akawaambia wafuasi wake, “Inatupasa kurudi tena Uyahudi.” Wakamjibu, “Lakini Mwalimu, ni muda mfupi tu uliopita viongozi wa Wayahudi pale walijitahidi kukuua kwa mawe. Sasa unataka kwenda huko tena?” Yesu akajibu, “Yako masaa kumi na mawili ya mchana katika siku. Yeyote anayetembea mchana hatajikwaa na kuanguka kwani anamulikiwa na nuru ya ulimwengu huu. Lakini yeyote anayetembea usiku atajikwaa kwa sababu hana nuru inayomwongoza.” Kisha Yesu akasema, “Rafiki yetu Lazaro sasa amelala, lakini nitakwenda ili nimwamshe.” Wafuasi wake wakajibu, “Lakini, Bwana, kama amelala ataweza kupona.” Walifikiri kwamba Yesu alikuwa na maana kwamba Lazaro alikuwa amelala usingizi, lakini Yeye alikuwa na maana kuwa amefariki. Kisha hapo Yesu akasema wazi wazi, “Lazaro amekufa. Na ninafurahi sikuwepo hapo. Ninafurahi kwa ajili yenu kwa sababu sasa mtaniamini mimi. Twendeni kwake sasa.” Ndipo Tomaso, pia aliyeitwa “Pacha”, akawaambia wafuasi wengine, “Nasi pia tutaenda kule kufa pamoja na Yesu.” Yesu akaenda Bethania na huko akakuta Lazaro amekufa na kuwa kaburini kwa siku nne. Mji wa Bethania ulikuwa kama kilomita tatu kutoka Yerusalemu. Wayahudi wengi wakaja ili kuwaona Martha na Mariamu. Walikuja ili kuwafariji kwa ajili ya msiba wa kaka yao, Lazaro. Martha aliposikia kuwa Yesu alikuwa anakuja, alikwenda kumpokea. Lakini Mariamu alibaki nyumbani. Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwepo hapa, ndugu yangu asingelikufa. Lakini najua kwamba hata sasa Mungu atakupa chochote utakachomwomba.” Yesu akasema, “Kaka yako atafufuka na kuwa hai tena.” Martha akajibu, “Ninajua kuwa atafufuka tena wakati wa ufufuo siku ya mwisho.” Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo. Mimi ndiye uzima. Kila anayeniamini atakuwa na uzima, hata kama atakufa. Kila atakayeniamini hatakufa kiroho hata kama atakufa kimwili. Je, Martha, unaliamini jambo hili?” Martha akajibu, “Ndiyo Bwana naliamini. Nakuamini kwamba wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu. Ndiwe unayekuja ulimwenguni.” Baada ya Martha kusema maneno haya, alirejea kwa Mariamu dada yake. Aliongea naye peke yake na kusema, “Mwalimu yupo hapa. Anakutafuta.” Mariamu aliposikia hivyo, aliinuka na kwenda haraka kwa Yesu. Yesu hakuwa amefika kijijini. Alikuwa bado yupo pale pale Martha alipomkuta. Wayahudi waliokuwepo nyumbani hapo wakimfariji Mariamu walimwona akiinuka na kuondoka ghafla. Walifikiri alikuwa anaenda kaburini kuomboleza. Hivyo wakamfuata. Mariamu alienda pale Yesu alipokuwa. Naye baada ya kumwona, aliinama miguuni pake Yesu na kusema, “Bwana, kama ungekuwa hapa, kaka yangu asingekufa.” Ndipo Yesu alipomwona Mariamu na watu waliokuwa pamoja naye wakilia, akahuzunika na kusikitika sana. Akawauliza, “Mmemweka wapi?” Wakasema, “Bwana, njoo uone.” Yesu akalia na kutoa machozi. Na Wayahudi wakasema, “Angalia! Alikuwa anampenda sana Lazaro!” Lakini wengine wao wakasema, “Yesu aliyeyaponya macho ya yule mtu asiyeona kwa nini hakumsaidia Lazaro na kumzuia asife?” Akiwa bado ana uchungu na kusikitika sana, Yesu akaenda kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa ni pango lenye jiwe kubwa lililofunika pa kuingilia. Yesu akasema, “Lisogezeni pembeni hilo jiwe.” Martha akasema, “Lakini, Bwana, ni siku nne sasa tangu Lazaro alipofariki. Kutakuwa na harufu mbaya.” Martha alikuwa ni dada wa marehemu. Kisha Yesu akamwambia Martha, “Unakumbuka jinsi nilivyokuambia? Je, sikukuambia kwamba kama ukiamini, ungeuona utukufu wa Mungu?” Kwa hiyo wakalisogeza lile jiwe kutoka kwenye sehemu ya kuingilia. Kisha Yesu akatazama juu na kusema, “Baba, Nakushukuru kwa kuwa ulinisikia. Najua kuwa siku zote unanisikia. Lakini nimeyasema mambo haya kwa ajili ya watu walioko hapa. Nataka kwamba waweze kuamini kuwa ni wewe uliyenituma.” Baada ya Yesu kusema hivi akaita kwa sauti kubwa, “Lazaro, toka nje!” Yule mtu aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa sanda. Uso wake ulikuwa umefunikwa kwa kitambaa. Yesu akawaambia watu, “Mfungueni hizo sanda na kumwacha aende.” Walikuwepo Wayahudi wengi waliokuja kumtembelea Mariamu. Hawa walipoona aliyotenda Yesu, wengi wao wakamwamini. Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwapa habari ya mambo aliyofanya Yesu. Kisha viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaitisha kikao cha baraza kuu. Wakasema, “Tutafanyaje? Mtu huyu anafanya ishara nyingi sana. Tukimwacha aendelee kufanya hivi, kila mtu atamwamini. Ndipo Warumi watakuja na kulichukua Hekalu na Taifa letu pia.” Mmoja wa watu wale alikuwa ni Kayafa. Yeye alikuwa kuhani mkuu kwa mwaka ule. Akasema, “Ninyi hamjui lo lote! Ni bora mtu mmoja akafa kwa ajili ya watu wengine badala ya taifa zima kuangamia. Ninyi bado hamjalitambua hili.” Kayafa hakufikiri hivi peke yake. Hakika kama kuhani mkuu kwa mwaka ule, alikuwa akitabiri kwamba Yesu angekufa kwa ajili ya Wayahudi. Kweli, angekufa kwa ajili ya Wayahudi. Lakini pia angekufa kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika ulimwenguni pote. Angekufa ili awakusanye na kuwaweka katika kundi moja. Siku ile viongozi wa Wayahudi wakaanza kupanga jinsi ya kumuua Yesu. Hivyo Yesu akaacha kusafiri wazi wazi katikati ya Wayahudi. Akaelekea katika mji ulioitwa Efraimu uliokuwa kwenye eneo karibu na jangwa. Akakaa huko pamoja na wafuasi wake. Wakati huo Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Watu wengi kutoka katika nchi yote ya Uyahudi wakaenda Yerusalemu siku chache kabla. Walienda kujitakasa tayari kwa ajili ya sikukuu hiyo. Watu wakamtafuta Yesu. Nao walisimama katika maeneo ya Hekalu na kuulizana, “Je, naye atakuja kwenye sikukuu? Unafikirije wewe?” Lakini viongozi wa makuhani na Mafarisayo walitoa agizo maalumu kuhusu Yesu. Walisema kuwa mtu yeyote anayejua mahali alipo Yesu awaambie ili waweze kumkamata. Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alienda Bethania. Huko ndiko alikoishi Lazaro, yule mtu aliyefufuliwa na Yesu kutoka wafu. Hapo walimwandalia Yesu karamu ya chakula. Naye Martha alihudumu na Lazaro alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakila chakula pamoja na Yesu. Mariamu akaleta manukato ya thamani sana yaliyotengenezwa kwa nardo asilia kwenye chombo chenye ujazo wa nusu lita hivi. Akayamwaga manukato hayo miguuni mwa Yesu. Kisha akaanza kuifuta miguu ya Yesu kwa nywele zake. Harufu nzuri ya manukato hayo ikajaa nyumba nzima. Yuda Iskariote, mmoja wa wafuasi wa Yesu, naye alikuwepo hapo. Yuda ambaye baadaye angemkabidhi Yesu kwa maadui zake akasema, “Manukato hayo yana thamani ya mshahara wa mwaka wa mtu. Bora yangeuzwa, na fedha hizo wangepewa maskini.” Lakini Yuda hakusema hivyo kwa vile alikuwa anawajali sana maskini. Alisema hivyo kwa sababu alikuwa mwizi. Naye ndiye aliyetunza mfuko wa fedha za wafuasi wa Yesu. Naye mara kadhaa aliiba fedha kutoka katika mfuko huo. Yesu akajibu, “Msimzuie. Ilikuwa sahihi kwake kutunza manukato haya kwa ajili ya siku ya leo; siku ambayo maziko yangu yanaandaliwa. Nyakati zote mtaendelea kuwa pamoja na hao maskini. Lakini si kila siku mtakuwa pamoja nami.” Wayahudi wengi wakasikia kwamba Yesu alikuwa Bethania, Kwa hiyo walienda huko ili wakamwone. Walienda pia ili kumwona Lazaro, yule ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu. Viongozi wa makuhani nao wakafanya mpango wa kumuua Lazaro. Walitaka kumwua kwa sababu, Wayahudi wengi waliwaacha makuhani hao na kumwamini Yesu. Siku iliyofuata watu waliokuwamo Yerusalemu walisikia kwamba Yesu alikuwa anakuja huko. Hili ni kundi la watu waliokuja kusherehekea sikukuu ya Pasaka. Hawa walibeba matawi ya miti ya mitende na kwenda kumlaki Yesu. Pia walipiga kelele wakisema, “‘Msifuni Yeye!’ ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye kwa jina la Bwana!’ Mungu ambariki Mfalme wa Israeli!” Yesu akamkuta punda njiani naye akampanda, kama vile Maandiko yanavyosema, “Msiogope, enyi watu wa Sayuni! Tazameni! Mfalme wenu anakuja. Naye amepanda mwana punda.” Wafuasi wa Yesu hawakuyaelewa yale yaliyokuwa yanatokea wakati huo. Lakini Yesu alipoinuliwa juu kwenye utukufu, ndipo walipoelewa kuwa haya yalitokea kama ilivyoandikwa juu yake. Kisha wakakumbuka kwamba walifanya mambo haya kwa ajili ya Yesu. Siku Yesu alipomfufua Lazaro kutoka wafu na kumwambia atoke kaburini walikuwepo watu wengi pamoja naye. Hawa walikuwa wakiwaeleza wengine yale aliyoyafanya Yesu. Ndiyo sababu watu wengi walienda ili kumlaki Yesu; kwa kuwa walikuwa wamesikia habari za ishara hii aliyoifanya. Mafarisayo nao wakasemezana wao kwa wao, “Tazameni! Mpango wetu haufanyi kazi. Watu wote wanamfuata Yesu!” Hapo Yerusalemu walikuwepo pia Wayunani. Hawa walikuwa ni miongoni mwa watu walioenda mjini humo kuabudu wakati wa sikukuu ya Pasaka. Hao walimwendea Filipo, aliyetoka Bethsaida kule Galilaya. Wakasema, “Bwana, tunahitaji kumwona Yesu.” Filipo alienda na kumwambia Andrea hitaji lao. Kisha Andrea na Filipo walienda na kumwambia Yesu. Yesu akawaambia Filipo na Andrea, “Wakati umefika kwa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu wake. Ni ukweli kwamba mbegu ya ngano inapaswa kuanguka katika ardhi na kuoza kabla ya kukua na kuzaa nafaka nyingi ya ngano. Kama haitakufa, haitaongezeka zaidi ya hiyo mbegu moja. Yeyote anayeyapenda maisha yake aliyonayo atayapoteza. Yeyote atakayetoa maisha yake kwa Yesu katika ulimwengu huu atayatunza. Nao wataupata uzima wa milele. Kama mtu atanitumikia inampasa anifuate. Watumishi wangu watakuwa pamoja nami popote nitakapokuwa. Mtu atakayenitumikia Baba yangu atamheshimu. Sasa ninapata taabu sana rohoni mwangu. Nisemeje? Je, niseme, ‘Baba niokoe katika wakati huu wa mateso’? Hapana, nimeufikia wakati huu ili nipate mateso. Baba yangu, ufanye yale yatakayokuletea wewe utukufu!” Kisha sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Tayari nimekwisha upata utukufu wangu. Nitaupata tena.” Watu waliokuwa wamesimama hapo wakaisikia sauti hiyo. Wakasema ilikuwa ni ngurumo. Lakini wengine wakasema, “Malaika amesema naye!” Yesu akasema, “Sauti hiyo ilikuwa ni kwa ajili yenu si kwa ajili yangu. Sasa ni wakati wa ulimwengu kuhukumiwa. Sasa mtawala wa ulimwengu huu atatupwa nje. Nami nitainuliwa juu kutoka katika nchi. Mambo hayo yatakapotokea, nitawavuta watu wote waje kwangu.” Yesu alisema hili kuonesha jinsi ambavyo atakufa. Watu wakasema, “Lakini sheria yetu inasema kwamba Masihi ataishi milele. Sasa kwa nini unasema, ‘Ni lazima Mwana wa Adamu ainuliwe juu’? Ni nani huyu ‘Mwana wa Adamu’?” Kisha Yesu akasema, “Nuru itabaki pamoja nanyi kwa muda mfupi tu. Kwa hiyo mtembee mkiwa bado na hiyo nuru. Hapo giza halitaweza kuwakamata. Watu wanaotembea gizani hawajui kule wanakoenda. Hivyo wekeni matumaini yenu katika nuru wakati bado mkiwa nayo. Jinsi hiyo mtakuwa watoto wa nuru.” Yesu alipomaliza kusema mambo hayo, aliondoka na kwenda mahali ambapo watu wasingeweza kumwona. Watu wakaona ishara hizi zote alizozifanya Yesu, lakini bado hawakumwamini. Haya yalikuwa hivyo ili kuthibitisha yale aliyoyasema nabii Isaya kuwa: “Bwana, ni nani aliyeamini yale tuliyowaambia? Ni nani aliyeziona nguvu za Bwana?” Hii ndiyo sababu watu hawakuweza kuamini. Kwani Isaya alisema pia, “Mungu aliwafanya baadhi ya watu wasione. Aliufunga ufahamu wao. Alifanya hivi ili wasiweze kuona kwa macho yao na kuelewa kwa ufahamu wao. Alifanya hivyo ili wasiweze kugeuka na kuponywa.” Isaya alisema hivi kwa sababu aliuona ukuu wa Mungu ndani ya Yesu. Naye alizungumza habari zake Yesu. Lakini watu wengi wakamwamini Yesu. Hata wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi wakamwamini, lakini walikuwa na hofu juu ya Mafarisayo, hivyo hawakusema kwa uwazi kwamba wameamini. Hao walikuwa na hofu kwamba wangeamriwa watoke na kukaa nje ya sinagogi. Wao walipenda kusifiwa na watu zaidi kuliko kupata sifa zinazotoka kwa Mungu. Kisha Yesu akapaza sauti, “Mtu yeyote anayeniamini basi kwa hakika anamwamini yule aliyenituma. Yeyote anayeniona mimi hakika anamwona yeye aliyenituma. Nimekuja katika ulimwengu huu kama mwanga. Nimekuja ili kila mmoja atakayeniamini asiendelee kuishi katika giza. Sikuja ulimwenguni humu kuwahukumu watu. Nimekuja ili kuwaokoa watu wa ulimwengu huu. Hivyo mimi siye ninayewahukumu wale wanaosikia mafundisho yangu bila kuyafuata. Isipokuwa yupo hakimu wa kuwahukumu wote wanaokataa kuniamini na wasiokubaliana na yale ninayoyasema. Ujumbe ninaousema utawahukumu ninyi siku ya mwisho. Hiyo ni kwa sababu yale niliyofundisha hayakutoka kwangu. Baba aliyenituma ndiye aliyeniambia yale nitakayosema na kuyafundisha. Nami najua amri za Mungu kwamba lolote alisemalo na kutenda litawaletea watu uzima wa milele, kama watazifanya. Hivyo mambo ninayosema ni yale ambayo Baba yangu ameniambia niyaseme.” Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Yesu alijua kwamba wakati wake wa kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ulikuwa umefika. Daima Yesu aliwapenda watu wa ulimwengu huu waliokuwa wake. Huu ulikuwa wakati alipowaonesha upendo wake mkuu. Yesu na wafuasi wake walikuwa wakila chakula cha jioni. Ibilisi alikuwa tayari amekwisha kumshawishi Yuda Iskariote kumsaliti Yesu kwa maadui zake. (Yuda alikuwa Mwana wa Simoni.) Baba alikuwa amempa Yesu uwezo juu ya kila kitu. Naye Yesu alilifahamu hili. Alijua pia kuwa yeye alitoka kwa Mungu. Tena alijua kuwa alikuwa anarudi kwa Mungu. Kwa hiyo walipokuwa wakila, Yesu alisimama na kulivua vazi lake. Akachukua taulo na kuifunga kiunoni mwake. Kisha akamimina maji katika bakuli na kuanza kuwaosha miguu wafuasi wake. Kisha akaifuta miguu yao kwa taulo aliolifunga kiunoni mwake. Akamfikia Simoni Petro, naye Simoni Petro akamwambia, “Bwana, huwezi kuiosha miguu yangu.” Yesu akamjibu, “Huyaelewi ninayofanya hivi sasa. Lakini utayaelewa baadaye.” Petro akasema, “Hapana! Huwezi kamwe kuniosha miguu yangu kamwe.” Yesu akamjibu, “Kama sitakuosha miguu yako, basi hutakuwa miongoni mwa watu wangu.” Simoni Petro akasema, “Bwana, utakapomaliza miguu, unioshe mikono na kichwa pia!” Yesu akamwambia, “Baada ya mtu kuoga, mwili wake wote huwa safi. Anahitaji tu kunawa miguu. Nanyi mko safi, lakini sio nyote.” Yesu alimjua yule atakayemsaliti mbele ya adui zake. Ndiyo maana alisema, “Sio wote mlio safi.” Yesu alipomaliza kuwaosha miguu wafuasi, alivaa nguo zake na kurudi pale mezani. Akawauliza, “Je, mmelielewa nililowafanyia? Mnaniita mimi ‘Mwalimu’. Tena mnaniita mimi ‘Bwana’. Hayo ni sahihi, kwa sababu hivyo ndivyo nilivyo. Mimi ni Bwana na Mwalimu wenu. Lakini niliwaosha miguu yenu kama mtumishi. Hivyo nanyi mnapaswa kuoshana miguu yenu. Nilifanya hivyo kama mfano. Hivyo nanyi mnapaswa kuhudumiana ninyi kwa ninyi kama nilivyowahudumia. Mniamini mimi, watumishi huwa sio wakubwa kuzidi bwana zao. Wale waliotumwa kufanya jambo fulani sio wakubwa kumzidi yule aliyewatuma. Sasa, mkielewa maana ya yale niliyotenda, Mungu atawabariki mkiyatendea kazi. Nami sizungumzii habari zenu nyote. Nawafahamu watu wale niliowachagua. Lakini Maandiko yanapaswa kutimia kama yanavyosema: ‘Mtu aliyekula chakula pamoja nami amenigeuka.’ Ninawaambia hili sasa kabla halijatokea. Hivyo litakapotokea, mtaweza kuamini kuwa MIMI NDIYE. Hakika nawaambieni, yeyote anayempokea mtu yule niliyemtuma ananipokea mimi pia. Na yeyote anayenipokea mimi humpokea pia yeye aliyenituma.” Baada ya Yesu kuyasema mambo haya, alisumbuka sana moyoni. Akasema kwa uwazi, “Mniamini ninaposema kwamba mmoja wenu atanisaliti kwa maadui zangu.” Wafuasi wake wote wakatazamana wao kwa wao. Hawakuelewa kuwa Yesu alikuwa anamzungumzia nani. Mmoja wa wafuasi wake alikaa karibu na Yesu na alikuwa amemwegemea. Huyu alikuwa yule aliyependwa sana na Yesu. Simoni Petro akaonyesha ishara kwa mfuasi huyo amwulize Yesu alikuwa anamzungumzia nani. Yule mfuasi alisogea karibu sana na Yesu na kumwuliza, “Bwana, ni nani huyo?” Yesu akamjibu, “Nitachovya mkate huu kwenye bakuli. Mtu yule nitakayempa mkate huo ndiye mwenyewe.” Kwa hiyo Yesu akachukua kipande cha mkate, akakichovya, na akampa Yuda Iskariote, Mwana wa Simoni. Yuda alipoupokea mkate ule, Shetani akamwingia. Yesu akamwambia Yuda, “Yale unayotaka kuyafanya, yafanye haraka!” Hakuna hata mmoja pale mezani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia Yuda hayo. Kwa vile Yuda ndiye aliyekuwa msimamizi wa fedha zao, baadhi yao walidhani kuwa Yesu alikuwa na maana kuwa Yuda aende kununua vitu ambavyo wangehitaji kwa ajili ya sherehe. Au walidhani kuwa Yesu alitaka Yuda aende na kuwapa maskini cho chote. Yuda akaula mkate aliopewa na Yesu. Kisha akatoka nje mara hiyo hiyo. Wakati huo ulikuwa ni usiku. Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa ni wakati wa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu. Na Mungu ataupokea utukufu kupitia kwake. Kama Mungu hupokea utukufu kupitia kwake, atampa Mwana Utukufu kupitia kwake yeye mwenyewe. Na hilo litatimia haraka sana.” Yesu akasema, “Watoto wangu, nitakuwa nanyi kwa kipindi kifupi tu kijacho. Nanyi mtanitafuta, lakini nawaambia sasa yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: Kule niendako ninyi hamwezi kuja.” “Nawapa amri mpya: Pendaneni ninyi kwa ninyi. Mnapaswa kupendana kama mimi nilivyowapenda ninyi. Endapo mtapendana ninyi kwa ninyi watu wote watatambua kuwa ninyi ni wafuasi wangu.” Simoni Petro akamwuliza Yesu, “Bwana, unaenda wapi?” Yesu akajibu, “Kule niendako hamwezi kunifuata sasa. Lakini mtanifuata baadaye.” Petro akauliza, “Bwana, kwa nini nisikufuate sasa? Mimi niko radhi kufa kwa ajili yako!” Yesu akajibu, “Je, ni kweli utayatoa maisha yako kwa ajili yangu? Hakika nakwambia, kabla jogoo hajawika, utasema mara tatu kwamba hunijui mimi.” Yesu akasema, “Msisumbuke. Mwaminini Mungu, na mniamini na mimi. Kuna vyumba vya kutosha katika nyumba ya Baba yangu. Nisingewaambia hivi ikiwa isingelikuwa kweli. Ninaenda huko kuandaa mahali kwa ajili yenu. Nitakapomaliza kuandaa, nitarudi. Kisha nitawachukua ili muwe pamoja nami mahali niliko. Mnaijua njia iendayo kule ninakokwenda.” Thomaso akasema, “Bwana, hatujui unakokwenda, sasa tutaijuaje njia?” Yesu akajibu, “Mimi ndiye njia, kweli, na uzima. Njia pekee ya kwenda kwa Baba ni kupitia kwangu. Kwa kuwa sasa ninyi nyote mmenijua, mtamjua Baba yangu pia. Kwa kweli, sasa mnamjua Baba na mmekwisha kumwona.” Filipo akamwambia, “Bwana, utuonyeshe Baba. Hilo tu ndilo tunalohitaji.” Yesu akajibu, “Nimekuwa pamoja nanyi kwa kipindi kirefu. Hivyo wewe, Filipo unapaswa kunijua. Yeyote aliyeniona mimi amemwona Baba pia. Hivyo kwa nini unasema, ‘Utuonyeshe Baba’? Hamwamini kuwa mimi nimo ndani ya Baba na Baba naye yumo ndani yangu? Mambo niliyowaambia hayatoki kwangu. Baba anakaa ndani yangu, naye anafanya kazi yake mwenyewe. Mniamini ninaposema kwamba nimo ndani ya Baba na Baba yumo ndani yangu. Vinginevyo muamini kwa sababu ya miujiza niliyoifanya. Hakika nawaambia, yeyote anayeniamini atafanya mambo kama yale niliyoyafanya. Naye atafanya mambo makubwa zaidi ya yale niliyofanya, kwa sababu mimi naenda kwa Baba. Na kama mtaomba jambo lo lote kwa jina langu, nitawafanyia. Kisha utukufu wa Baba utadhihirishwa kupitia kwa Mwana wake. Ikiwa mtaniomba chochote kwa jina langu, mimi nitakifanya. Ikiwa mnanipenda, mtafanya ninayowaagiza. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine atakayekuwa nanyi siku zote. Huyo Msaidizi ni Roho wa Kweli ambaye watu wa ulimwengu hawawezi kumpokea, kwa sababu hawamwoni wala hawamjui. Lakini ninyi mnamjua kwa kuwa anakaa pamoja nanyi, na atakuwa ndani yenu. Mimi sitawaacha peke yenu kama watu wasiokuwa na wazazi. Bali nitakuja tena kwenu. Katika kipindi kifupi watu wa ulimwengu hawataniona tena. Lakini ninyi mtaniona. Mtaishi kwa sababu mimi ninaishi. Katika siku hiyo mtaelewa kuwa mimi nimo ndani ya Baba. Kadhalika mtajua pia kuwa ninyi mmo ndani yangu nami nimo ndani yenu. Wale wanaonipenda kweli ni wale ambao si tu kwamba wanazijua amri zangu bali pia wanazitii. Baba yangu atawapenda watu wa jinsi hiyo, nami pia nitawapenda. Nami nitajitambulisha kwao.” Kisha Yuda (siyo Yuda Iskariote) akasema, “Bwana, utawezaje kujitambulisha kwetu, lakini si kwa ulimwengu?” Yesu akajibu, “Wale wote wanipendao watayafuata mafundisho yangu. Naye Baba yangu atawapenda. Kisha Baba yangu na mimi tutakuja kwao na kukaa pamoja nao. Lakini yeyote asiyenipenda hafuati mafundisho yangu. Mafundisho haya mnayosikia kwa hakika siyo yangu. Ni kutoka kwa Baba yangu aliyenituma. Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. Lakini yule Msaidizi atawafundisha kila kitu na kuwafanya mkumbuke kila nilichowaambia. Huyu Msaidizi ni Roho Mtakatifu ambaye Baba atamtuma kwa jina langu. Nawaachia amani. Ninawapa amani yangu mwenyewe. Ninawapa amani kwa namna tofauti kabisa na jinsi ulimwengu unavyofanya. Hivyo msihangaike. Msiogope. Mlinisikia nikiwaambia, ‘Naondoka, lakini nitakuja tena kwenu.’ Mngenipenda, mngefurahi kuwa naenda kwa Baba, kwa sababu Baba ni mkuu kuliko mimi. Nawaambia haya hivi sasa, kabla hayajatokea. Kisha yatakapotokea, mtaamini. Sitaendelea kuongea nanyi kwa muda mrefu zaidi. Mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Hata hivyo hana nguvu juu yangu. Lakini ni lazima ulimwengu utambue kuwa ninampenda Baba. Hivyo ninafanya yale Baba aliyoniambia. Njooni sasa, twendeni.” Yesu akasema, “Mimi ndiye mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Yeye hulikata kutoka kwangu kila tawi lisilozaa matunda. Pia hupunguza majani katika kila tawi linalozaa matunda ili kuliandaa liweze kuzaa matunda zaidi. Ninyi mmewekwa tayari kwa ajili ya kuzaa matunda kutokana na mafundisho yale niliyowapa. Hivyo mkae mkiwa mmeunganishwa kwangu, nami nitakaa nikiwa nimeunganishwa kwenu. Hakuna tawi linaloweza kuzaa matunda likiwa liko peke yake. Ni lazima liwe limeunganishwa katika mzabibu. Ndivyo ilivyo hata kwenu. Hamwezi kutoa matunda mkiwa peke yenu. Ni lazima muwe mmeunganishwa kwangu. Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Mtatoa matunda mengi sana mkiwa mmeunganishwa kwangu, nami nimeunganishwa kwenu. Lakini mkitenganishwa mbali nami hamtaweza kufanya jambo lo lote. Kama hamtaunganishwa nami, basi mtakuwa sawa na tawi lililotupwa pembeni nanyi mtakauka. Matawi yote yaliyokufa jinsi hiyo hukusanywa, hutupwa katika moto na kuchomwa. Hivyo ninyi mbaki mmeunganishwa nami, na mfuate mafundisho yangu. Mkifanya hivyo, mnaweza kuomba kitu chochote mnachohitaji, nanyi mtapewa. Ninyi mdhihirishe kuwa mmekuwa wafuasi wangu kwa kutoa matunda mengi. Kwani hiyo itamletea Baba utukufu. Mimi nimewapenda kama vile Baba alivyonipenda. Sasa mdumu katika upendo wangu. Nimezitii amri za Baba yangu, naye anaendelea kunipenda. Kwa jinsi hiyo, nami nitaendelea kuwapenda mkizitii amri zangu. Nimewaambia haya ili mpate furaha ya kweli kama ile niliyonayo mimi. Nami ninatamani muwe na furaha iliyo kamilifu. Hii ndiyo amri yangu kwenu: Mpendane ninyi kwa ninyi kama mimi nilivyowapenda. Hakuna anayeweza kuonesha pendo lolote kuu zaidi ya kuwa tayari kufa kwa ajili ya rafiki zake. Upendo wa hali ya juu unaoweza kuoneshwa na watu ni kufa badala ya rafiki zao. Nanyi ni rafiki zangu mnapoyafanya yale ninayowaambia myafanye. Siwaiti tena watumwa, kwa sababu watumwa hawajui yale yanayofanywa na bwana zao. Lakini sasa nawaita marafiki, kwa sababu nimewaambia yote aliyoniambia Baba yangu. Ninyi hamkunichagua mimi. Bali ni mimi niliyewachagua ninyi. Nami niliwapa kazi hii: Kwenda na kutoa matunda; matunda ambayo yatadumu. Ndipo Baba atakapowapa chochote mtakachomwomba katika jina langu. Hii ndiyo amri yangu: Mpendane ninyi kwa ninyi. Endapo ulimwengu utawachukia, mkumbuke kwamba umenichukia mimi kwanza. Kama mngekuwa wa ulimwengu huu, ulimwengu ungewapenda kama watu wake. Lakini ulimwengu unawachukia kwa sababu ninyi siyo wa ulimwengu huu. Badala yake, mimi niliwachagua ninyi ili muwe tofauti na ulimwengu. Kumbukeni somo nililowafundisha: Watumwa sio wakubwa kuliko mabwana wao. Kama watu walinitendea mimi vibaya, watawatendea vibaya hata nanyi pia. Na kama waliyatii mafundisho yangu, watayatii hata ya kwenu pia. Watawatendea yale waliyonitendea mimi, kwa sababu ninyi ni wangu. Wao hawamjui yeye aliyenituma. Kama nisingekuwa nimekuja na kusema na watu wa ulimwengu, basi wasingekuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa nimekwisha sema nao. Hivyo hawana cha kisingizio cha dhambi zao. Yeyote anayenichukia mimi anamchukia na Baba pia. Mimi nilifanya mambo miongoni mwa watu wa ulimwengu ambayo hayajawahi kufanywa na mtu yeyote mwingine. Kama nisingefanya mambo hayo, wao nao wasingekuwa na hatia ya dhambi. Ijapokuwa waliyaona niliyofanya, bado wananichukia mimi na Baba yangu. Lakini haya yalitokea ili kuweka wazi yaliyoandikwa katika sheria zao: ‘Walinichukia bila sababu yoyote.’” Mimi, “Nitamtuma Msaidizi kutoka kwa Baba. Huyo Msaidizi ni Roho wa kweli anayekuja kutoka kwa Baba. Yeye atakapokuja, atasema juu yangu. Nanyi pia mtawajulisha watu juu yangu, kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo. Nimewaambia mambo haya yote ili msipoteze imani mtakapokutana na matatizo. Watu watawafukuza mtoke katika masinagogi na msirudi humo tena. Hakika, unakuja wakati watapofikiri kuwa kwa kuwaua ninyi watakuwa wanatoa huduma kwa Mungu. Watafanya hivyo kwa sababu hawajamjua Baba, na hawajanijua mimi pia. Nimewaambia haya sasa ili kuwaandaa. Hivyo wakati wa mambo haya kutimia utakapofika, mtakumbuka kwamba niliwapa tahadhari mapema. Sikuwaambia mambo haya tangu mwanzo, kwa sababu bado nilikuwa pamoja nanyi. Sasa narudi kwake yeye aliyenituma, ingawa hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza, ‘Unakwenda wapi?’ Nanyi mmejawa na huzuni kwa vile nimewaambia mambo haya yote. Hakika nawaambieni, ni kwa faida yenu mimi nikiondoka. Nasema hivi kwa sababu, nitakapoondoka nitamtuma kwenu Msaidizi. Lakini nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja. Ila huyo Msaidizi atakapokuja, atawaonesha watu wa ulimwengu jinsi walivyofanya dhambi. Atawaonesha nani ana hatia ya dhambi, nani ana haki mbele za Mungu, na nani anastahili kuhukumiwa na Mungu. Huyo Msaidizi atawaonesha kuwa wana hatia ya dhambi kwa sababu hawaniamini mimi. Atawaonesha jinsi wasivyoelewa mtu anavyohesabiwa haki na Mungu. Hakika mimi nina kibali kwa sababu naenda kwa Baba nanyi hamtaniona tena. Naye atawaonesha watu wa ulimwengu huu jinsi hukumu yao isivyo sahihi, kwa sababu mkuu wao ulimwenguni amekwisha hukumiwa. Ninayo mambo mengi ya kuwaeleza, lakini ni magumu kwenu kuyapokea kwa sasa. Hata hivyo atakapokuja huyo Roho wa kweli, Yeye atawaongoza hadi kwenye kweli yote. Hatasema maneno yake mwenyewe bali atayasema yale tu anayosikia na atawajulisha yale yatakayotokea baadaye. Roho wa kweli atanipa mimi utukufu kwa kuwaeleza ninyi yote aliyopokea kutoka kwangu. Yote aliyonayo Baba ni yangu pia. Ndiyo sababu nilisema kwamba Roho atawaeleza yote anayopokea kutoka kwangu. Baada ya kipindi kifupi hamtaniona. Kisha baada ya kipindi kingine kifupi mtaniona tena.” Baadhi ya wafuasi wake wakaambiana wao kwa wao, “Ana maana gani anaposema, ‘Baada ya kipindi kifupi hamtaniona tena. Kisha baada ya kipindi kifupi kingine mtaniona tena?’ Tena ana maana gani anaposema, ‘Kwa sababu naenda kwa Baba’?” Wakauliza pia, “Ana maana gani anaposema ‘Kipindi kifupi’? Sisi hatuelewi anayosema.” Yesu alitambua kuwa wafuasi wake walitaka kumwuliza juu ya jambo hilo. Hivyo akawaambia, “Je, mnaulizana ninyi kwa ninyi kwamba nilikuwa na maana gani niliposema, ‘Baada ya kipindi kifupi hamtaniona. Kisha baada ya kipindi kifupi kingine mtaniona tena’? Hakika nawaambia, ninyi mtapata huzuni na kulia, bali ulimwengu utakuwa na furaha. Ndio, mtapata huzuni, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. Mwanamke anapojifungua mtoto, hupata maumivu, kwa sababu wakati wake umefika. Lakini baada ya mtoto kuzaliwa, huyasahau maumivu yale. Husahau kwa sababu huwa na furaha kwa kuwa mtoto amezaliwa ulimwenguni. Ndivyo ilivyo hata kwenu pia. Sasa mna huzuni lakini nitawaona tena, nanyi mtafurahi. Mtakuwa na furaha ambayo hakuna mtu atakayewaondolea. Katika siku hiyo, hamtapaswa kuniuliza mimi kitu chochote. Nami kwa hakika nawaambia, Baba yangu atawapa lo lote mtakalomwomba kwa jina langu. Hamjawahi kuomba lo lote kwa namna hii hapo awali. Bali ombeni kwa jina langu nanyi mtapewa. Kisha mtakuwa na furaha iliyotimia ndani yenu. Nimewaambia mambo haya kwa kutumia maneno yenye mafumbo. Isipokuwa utakuja wakati ambapo sitatumia tena maneno ya jinsi hiyo kuwaeleza mambo. Nami nitasema nanyi kwa maneno ya wazi wazi juu ya Baba. Kisha, mtaweza kumwomba Baba vitu kwa jina langu. Sisemi kwamba nitapaswa kumwomba Baba kwa ajili yenu. Baba mwenyewe anawapenda kwa sababu ninyi mmenipenda mimi. Naye anawapenda kwa sababu mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. Mimi nimetoka kwa Baba kuja ulimwenguni. Sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.” Kisha wafuasi wake wakasema, “Tayari unaongea nasi wazi wazi. Hutumii tena maneno yanayoficha maana. Sasa tunatambua kuwa unajua mambo yote. Wewe unajibu maswali yetu hata kabla hatujayauliza. Hii inatufanya tuamini kwamba ulitoka kwa Mungu.” Yesu akasema, “Kwa hiyo sasa mnaamini? Basi nisikilizeni! Wakati unakuja mtakapotawanywa, kila mmoja nyumbani kwake. Kwa hakika, wakati huo tayari umekwisha fika. Ninyi mtaniacha, nami nitabaki peke yangu. Lakini kamwe mimi siko peke yangu, kwa sababu Baba yupo pamoja nami. Nimewaambia mambo haya ili muwe na amani ndani yangu. Katika ulimwengu huu mtapata mateso. Lakini muwe jasiri! Mimi nimeushinda ulimwengu!” Baada ya Yesu kusema maneno hayo, alitazama mbinguni na kuomba, “Baba, wakati umefika. Mpe utukufu Mwanao ili Mwanao naye akupe wewe utukufu. Ulimpa Mwana mamlaka juu ya watu wote ili awape uzima wa milele wale wote uliompa. Na uzima wa milele ndiyo huu: kwamba watu watakujua wewe, Mungu pekee wa kweli, na kwamba watamjua Yesu Kristo, Yeye uliyemtuma. Mimi nimeimaliza kazi uliyonipa niifanye. Nami nimekupa utukufu duniani. Sasa, Bwana, unipe utukufu wako niwe nao pamoja nawe, utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya kuumbwa ulimwengu. Wewe ulinipa baadhi ya wafuasi kutoka watu wa ulimwengu huu. Hao nimewaonesha jinsi wewe ulivyo. Walikuwa watu wako, lakini ukawakabidhi kwangu. Wao wameyashika mafundisho yako. Sasa wanajua kuwa kila kitu nilichonacho kimetoka kwako. Mimi niliwaeleza maneno uliyonipa, nao wakayapokea. Walitambua ukweli kuwa mimi nilitoka kwako na wakaamini kuwa wewe ndiye uliyenituma. Mimi ninawaombea hao sasa. Siwaombei watu walioko ulimwenguni. Bali nawaombea wale watu ulionipa, kwa sababu hao ni wako. Vyote nilivyo navyo ni vyako, na vyote ulivyo navyo ni vyangu. Kisha utukufu wangu umeonekana ndani yao. Sasa nakuja kwako. Mimi sitakaa ulimwenguni, lakini hawa wafuasi wangu bado wamo ulimwenguni. Baba Mtakatifu, uwaweke hao salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Ndipo watapokuwa na umoja, kama vile mimi na wewe tulivyo. Nilipokuwa pamoja nao niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Niliwalinda. Ni mmoja wao tu aliyepotea; yule ambaye kwa hakika angelikuja kupotea. Hii ilikuwa hivyo ili kuonesha ukweli wa yale yaliyosemwa na Maandiko kuwa yangetokea. Nami nakuja kwako sasa. Lakini maneno haya nayasema ningali nimo ulimwenguni ili wafuasi hawa wawe na furaha kamili ndani yao. Nimewapa mafundisho yako. Nao ulimwengu umewachukia, kwa sababu wao sio wa ulimwengu, kama mimi nisivyokuwa wa ulimwengu. Siombi kwamba uwaondoe katika ulimwengu. Bali ninaomba uwalinde salama kutoka kwa Yule Mwovu. Wao si wa ulimwengu huu, kama mimi nisivyokuwa wa ulimwengu huu. Kupitia kweli yako uwatayarishe kwa utumishi wako. Mafundisho yako ndiyo kweli. Mimi nimewatuma ulimwenguni, kama wewe ulivyonituma mimi ulimwenguni. Nami najiweka tayari kabisa kukutumikia wewe. Ninafanya hivi kwa ajili yao ili wao nao wawe wamekamilika kukutumikia. Siwaombei tu hao wafuasi wangu lakini nawaombea pia wale watakaoniamini kutokana na mafundisho yao. Baba, naomba kwamba wote wanaoniamini waungane pamoja na kuwa na umoja. Wawe na umoja kama vile wewe na mimi tulivyoungana; wewe umo ndani yangu nami nimo ndani yako. Nami naomba nao pia waungane na kuwa na umoja ndani yetu. Ndipo ulimwengu nao utaamini kuwa ndiwe uliyenituma. Mimi nimewapa utukufu ule ulionipa. Nimewapa utukufu huo ili wawe na umoja, kama mimi na wewe tulivyo na umoja. Nitakuwa ndani yao, nawe utakuwa ndani yangu. Hivyo watakuwa na umoja kamili. Kisha ulimwengu utajua kwamba wewe ndiwe uliyenituma na ya kuwa uliwapenda jinsi ulivyonipenda mimi. Baba, ninataka hawa watu ulionipa wawe nami mahali pale nitakapokuwa. Nataka wauone utukufu wangu, utukufu ule ulionipa kwa sababu ulinipenda kabla ulimwengu haujaumbwa. Baba wewe ndiye unayetenda yaliyo haki. Ulimwengu haukujui, bali mimi nakujua, na hawa wafuasi wangu wanajua kuwa wewe ndiye uliyenituma. Nimewaonesha jinsi ulivyo, na nitawaonesha tena. Kisha watakuwa na upendo ule ule ulio nao wewe kwangu, nami nitaishi ndani yao.” Yesu alipomaliza kuomba, akaondoka pamoja na wafuasi wake kwenda ng'ambo kuvuka bonde la Kidroni. Akaenda katika bustani mahali hapo, akiwa bado pamoja na wafuasi wake. Yuda, yule aliyehusika kumsaliti Yesu, alipafahamu mahali pale. Alipajua kwa sababu Yesu mara nyingi alikutana na wafuasi wake pale. Kwa hiyo Yuda akaongoza kundi la askari hadi katika bustani hiyo pamoja na walinzi wengine kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Hawa walikuwa wamebeba mienge, taa, na silaha. Yesu alikwisha kujua yote ambayo yangempata. Hivyo aliwaendea na kuwauliza, “Je, ni nani mnayemtafuta?” Wakamjibu, “Yesu kutoka Nazareti.” Akawaambia, “Mimi ni Yesu.” (Yuda yule aliyehusika kumsaliti Yesu alikuwa amesimama hapo pamoja nao.) Yesu aliposema, “Mimi ni Yesu,” wale watu walirudi nyuma na kuanguka chini. Akawauliza tena, “Je, ni nani mnayemtafuta?” Wakasema, “Yesu kutoka Nazareti.” Yesu akasema, “Nimewaambia kwamba mimi ndiye Yesu. Hivyo kama mnanitafuta mimi, basi waacheni huru watu hawa waende zao.” Hii ilikuwa kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu mapema: “Sikumpoteza hata mmoja wa wale ulionipa.” Simoni Petro akauchomoa upanga aliokuwa ameufunga kiunoni. Akampiga nao mtumishi wa Kuhani Mkuu, na kulikata sikio lake la kulia. (Jina la mtumishi huyo lilikuwa ni Maliko.) Yesu akamwambia Petro, “Rudisha jambia lako mahali pake! Ninapaswa kunywa toka kikombe ambacho Baba amenipa nikinywee.” Kisha askari hao pamoja na mkuu wao na walinzi wa Kiyahudi wakamkamata Yesu. Wakamfunga, nao wakampeleka kwanza kwa Anasi, baba mkwe wa Kayafa. Kayafa alikuwa Kuhani Mkuu kwa mwaka huo. Naye ndiye aliyewashauri viongozi wengine wa Kiyahudi kwamba ingemfaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu wote. Simoni Petro na mmoja wa wafuasi wengine wa Yesu walienda pamoja na Yesu. Mfuasi huyu alimfahamu kuhani mkuu. Hivyo akaingia pamoja na Yesu ndani ya uwanja wa nyumba ya kuhani mkuu. Lakini Petro alisubiri nje karibu na mlango. Yule mfuasi aliyemjua kuhani mkuu alirudi nje na kuongea na mlinda mlango. Kisha alimleta Petro ndani. Msichana aliyekuwepo langoni alimwambia Petro, “Je! Wewe pia ni mmoja wa wafuasi wa mtu yule?” Petro akajibu, “Hapana, mimi siye!” Ilikuwa baridi, hivyo watumishi na walinzi waliwasha moto wa kuni. Walikuwa wameuzunguka, wakipasha joto miili yao naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao. Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu maswali kuhusu wafuasi wake pamoja na mafundisho aliyowapa. Yesu akamjibu, “Daima nimesema wazi kwa watu wote. Siku zote nimefundisha kwenye masinagogi na kwenye eneo la Hekalu. Wayahudi wote hukusanyika pale. Sijawahi kusema jambo lo lote kwa siri. Sasa kwa nini unaniuliza? Waulize watu waliosikia mafundisho yangu. Wao wanajua niliyosema!” Yesu aliposema hivyo, mmoja wa walinzi aliyekuwa amesimama hapo akampiga. Mlinzi huyo akasema, “Hupaswi kusema hivyo kwa kuhani mkuu!” Yesu akajibu, “Kama nimesema vibaya jambo lo lote, mwambie kila mtu hapa kosa lenyewe. Lakini kama niliyosema ni sahihi, kwa nini basi unanipiga?” Hivyo Anasi akampeleka Yesu kwa Kayafa kuhani mkuu. Naye alikuwa bado amefungwa. Simoni Petro alikuwa amesimama karibu na moto, akijipasha joto. Watu wengine wakamwambia Petro, “Je, wewe si mmoja wa wafuasi wa mtu yule?” Petro alikataa hilo. Akasema, “Hapana, mimi siye.” Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu alikuwapo pale. Naye alikuwa ni jamaa wa mtu yule aliyekatwa sikio na Petro. Mtumishi akamwambia Petro, “Nadhani nilikuona pamoja naye pale kwenye bustani!” Lakini kwa mara nyingine Petro akasema, “Hapana, sikuwa pamoja naye!” Mara tu alipomaliza kusema hayo, jogoo akawika. Kisha walinzi wakamchukua Yesu kutoka katika nyumba ya Kayafa kwenda kwenye jumba la mtawala wa Kirumi. Nayo ilikuwa ni mapema asubuhi. Wayahudi waliokuwa pale wasingeweza kuingia ndani ya jumba hilo. Wao hawakutaka kujinajisi wenyewe kwa sababu walitaka kuila karamu ya Pasaka. Kwa hiyo Pilato akatoka nje kuwafuata na akawauliza, “Mnasema mtu huyu amefanya makosa gani?” Wakajibu, “Yeye ni mtu mbaya. Ndiyo maana tumemleta kwako.” Pilato akawaambia, “Mchukueni wenyewe na kumhukumu kufuatana na sheria yenu.” Viongozi wa Wayahudi wakamwambia, “Lakini sheria yako haituruhusu sisi kumwadhibu mtu yeyote kwa kumwua.” (Hii ilikuwa ni kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu juu ya jinsi ambavyo angekufa.) Kisha Pilato alirudi ndani ya jumba lile. Aliagiza Yesu aje na akamuuliza, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Je, hilo ni swali lako mwenyewe au watu wengine wamekuambia juu yangu?” Pilato akajibu, “Mimi sio Myahudi! Ni watu wako mwenyewe na viongozi wa makuhani waliokuleta kwangu. Je, umefanya kosa gani?” Yesu akajibu, “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ungekuwa hivyo, watumishi wangu wangenipigania ili nisikabidhiwe kwa viongozi wa Wayahudi. Hapana, ufalme wangu sio wa kidunia.” Pilato akasema, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Yesu akamjibu, “Uko sahihi unaposema kuwa mimi ni mfalme. Nami nilizaliwa kwa ajili ya hili: kuwaeleza watu juu ya kweli. Ni kwa sababu hii nalikuja ulimwenguni. Kila mmoja aliye wa upande wa kweli hunisikiliza.” Pilato akasema, “Kweli ndiyo nini?” Kisha alitoka nje tena kwenda kwa viongozi wa Wayahudi na kuwaimbia, “Mimi sipati kitu chochote kibaya cha kumpinga mtu huyu. Lakini ni moja ya desturi zenu kwangu mimi kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi’?” Wakajibu kwa kupiga kelele wakisema, “Hapana, siyo yeye! Mwache huru Baraba!” (Baraba alikuwa jambazi.) Kisha Pilato akaamuru Yesu aondolewe akachapwe viboko. Askari wakatengeneza taji kutokana na matawi yenye miiba na kuiweka kichwani kwake. Kisha wakamzungushia vazi la rangi ya zambarau mwilini mwake. Wakaendelea kumkaribia wakisema, “Salamu kwako mfalme wa Wayahudi!” Kisha wakampiga Yesu usoni. Kwa mara nyingine Pilato alienda nje na kuwaambia viongozi wa Wayahudi, “Tazameni! Ninamtoa nje Yesu na kumleta kwenu. Ninataka mfahamu kuwa sijapata kwake jambo lolote ambalo kwa hilo naweza kumshitaki.” Kisha Yesu akatoka nje akiwa amevishwa taji ya miiba na vazi la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu ndiye mtu mwenyewe!” Viongozi wa makuhani na walinzi wa Kiyahudi walipomwona Yesu wakapiga kelele, “Mpigilieni misumari msalabani! Mpigilieni misumari msalabani!” Lakini Pilato akajibu, “Mchukueni na mpigilieni msalabani ninyi wenyewe. Mimi sioni kosa lolote la kumshitaki.” Viongozi wa Wayahudi wakasema, “Tunayo sheria inayosema kuwa ni lazima afe, kwa sababu alisema kuwa yeye ni Mwana wa Mungu.” Pilato aliposikia haya, aliogopa zaidi. Hivyo akarudi ndani ya jumba lake na kumwuliza Yesu, “Wewe unatoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu kitu. Pilato akasema, “Unakataa kusema nami? Kumbuka, ninao uwezo wa kukuweka huru au kukuua msalabani.” Yesu akajibu, “Uwezo pekee ulio nao juu yangu ni ule uwezo uliopewa na Mungu. Kwa hiyo yule aliyenitoa mimi kwenu anayo hatia ya dhambi kubwa zaidi.” Baada ya hayo, Pilato alijaribu kumwacha huru Yesu. Lakini viongozi wa Wayahudi wakapiga kelele, “Yeyote anayejiweka mwenyewe kuwa mfalme yuko kinyume cha Kaisari. Hivyo kama utamwacha huru mtu huyu, hiyo itakuwa na maana kuwa wewe si rafiki wa Kaisari.” Pilato aliposikia maneno hayo, akamtoa nje Yesu na kumweka mahali palipoitwa “Sakafu ya Mawe.” (Kwa Kiaramu jina lake ni Gabatha.) Pale Pilato akaketi katika kiti cha hakimu. Wakati huu, ilikuwa imekaribia kuwa saa sita adhuhuri katika Siku ya Matayarisho ya juma la Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!” Wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Mwue msalabani!” Pilato akawauliza, “Mnanitaka nimwue mfalme wenu msalabani?” Viongozi wa makuhani wakajibu, “Kaisari ndiye Mfalme pekee tuliye naye!” Hivyo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili auawe juu ya msalaba. Askari wakamchukua Yesu. Naye Yesu akaubeba msalaba wake hadi mahali panapoitwa “Fuvu la Kichwa”. (Kwa Kiaramu mahali hapo paliitwa “Golgotha”.) Hapo wakampigilia Yesu kwa misumari katika msalaba. Pia wakawapigilia kwa misumari watu wengine wawili kwenye misalaba miwili tofauti. Kila mmoja akawekwa pembeni upande wa kushoto na kuume wa msalaba wa Yesu naye akawa katikati yao. Pilato akawaambia waandike kibao na kisha kukiweka juu ya msalaba. Kibao hicho kiliandikwa na kilisema, “YESU WA NAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.” Kibao hicho kiliandikwa kwa Kiaramu, Kirumi na Kiyunani. Wayahudi walio wengi walikisoma kibao hicho, kwa sababu mahali ambapo Yesu alipigiliwa kwa misumari msalabani palikuwa karibu na mji. Viongozi wa makuhani wa Kiyahudi wakamwambia Pilato, “Usiandike, ‘Mfalme wa Wayahudi.’ Bali andika, ‘Mtu huyu alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’” Pilato akawajibu, “Sitayabadili yale niliyokwisha kuyaandika.” Hivyo baada ya askari kumpigilia Yesu kwa misumari msalabani, walizichukua nguo zake na kuzigawa katika mafungu manne. Kila askari alipata fungu moja. Pia wakalichukua vazi lake lililokuwa limefumwa kwa kipande kimoja tu cha kitambaa kutoka juu hadi chini. Hivyo askari wakasemezana wao kwa wao, “Hatutalichana vazi hili vipande vipande. Hebu tulipigie kura kuona nani atakayelipata.” Hili lilitokea ili kuweka wazi maana kamili ya yale yanayosemwa katika Maandiko: “Waligawana miongoni mwao mavazi yangu, na wakakipigia kura kile nilichokuwa nimevaa.” Hivyo ndivyo maaskari walivyofanya. Mama yake Yesu alisimama karibu na msalaba wa mwanawe, Dada yake mamaye Yesu pia alikuwa amesimama pale pamoja na Mariamu mke wake Kleopa, na Mariamu Magdalena. Yesu akamwona mama yake na akamwona pia mfuasi aliyempenda sana akisimama pale. Akamwambia mama yake, “Mama mpendwa, mwangalie huyo, naye ni mwanao sasa.” Kisha akamwambia yule mfuasi, “Huyu hapa ni mama yako sasa.” Kisha baada ya hayo, mfuasi huyo akamchukua mama yake Yesu na kuishi naye nyumbani kwake. Baadaye, Yesu akajua kuwa kila kitu kimekwisha kamilika. Ili kuyafanya Maandiko yatimie akasema, “Nina kiu.” Palikuwapo na bakuli lililojaa siki mahali pale, wale askari wakachovya sponji ndani yake. Wakaiweka ile sponji kwenye tawi la mwanzi na kuliinua hadi kinywani kwa Yesu. Alipoionja ile siki, akasema, “Imekwisha.” Baada ya hapo akainamisha kichwa chake na kufa. Hii ilikuwa Ijumaa, Siku ya Matayarisho. Siku iliyofuata ilikuwa ni siku ya Sabato maalumu. Viongozi wa Kiyahudi hawakuitaka ile miili ya waliosulubiwa ikae juu misalabani katika siku ya Sabato. Hivyo wakamwomba Pilato atoe amri kuwa miguu ya wale watu misalabani ivunjwe. Pia wakaomba ile miili ishushwe kutoka kwenye misalaba. Kwa hiyo askari wakaja na kuivunja miguu ya watu wale wawili kwenye misalaba kando ya Yesu. Lakini askari walipomkaribia Yesu, wakaona kuwa tayari alikuwa amekwisha kufa. Hivyo hawakuivunja miguu yake. Lakini mmoja wa askari akauchoma ubavu wa Yesu kwa mkuki wake. Mara hiyo hiyo damu na maji vikamtoka mwilini mwake. (Yeye aliyeona haya yakitokea ametueleza. Aliyaeleza haya ili ninyi pia muweze kuamini. Mambo anayosema ni ya kweli. Yeye anajua kuwa anasema kweli.) Mambo haya yalitokea ili kutimiza Maandiko yaliyosema, “Hakuna mfupa wake utakaovunjwa” na “Watu watamwangalia yeye waliyemchoma.” Baadaye, mtu mmoja aliyeitwa Yusufu wa kutoka Arimathaya akamwomba Pilato mwili wa Yesu. (Yusufu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini hakumweleza mtu yeyote, kwa sababu aliwaogopa viongozi wa Kiyahudi.) Pilato akasema Yusufu anaweza kuuchukua mwili wa Yesu, hivyo naye akaja na kuuchukua. Nikodemu akaenda pamoja na Yusufu. Nikodemu, alikuwa ni yule mtu aliyekuja kwa Yesu hapo kabla na kuzungumza naye usiku. Huyu alileta kadiri ya lita mia moja ya marashi yenye mchanganyiko wa manemane na uvumba. Watu hawa wawili wakauchukua mwili wa Yesu na wakauzungushia vipande vya sanda ya kitani pamoja na marashi yale. (Hivi ndivyo Wayahudi walivyowazika watu.) Pale msalabani sehemu alipouawa Yesu, palikuwepo na bustani. Katika bustani ile palikuwemo na kaburi jipya la kuzikia. Hakuna mtu aliyewahi kuzikwa ndani ya kaburi lile. Wanaume wakauweka mwili wa Yesu katika kaburi lile kwa kuwa lilikuwa karibu, na Wayahudi walikuwa wakijiandaa kuianza siku yao ya Sabato. Asubuhi na mapema siku ya Jumapili, wakati bado lilikuwepo giza, Mariamu Magdalena akaenda kwenye kaburi la Yesu. Naye akaona kuwa lile jiwe kubwa lilikuwa limeondolewa kutoka mlangoni. Hivyo akakimbia kwenda kwa Simoni Petro na kwa mfuasi mwingine (yule ambaye Yesu alimpenda sana). Akasema, “Wamemwondoa Bwana kutoka kaburini na hatujui wamemweka wapi.” Kwa hiyo Petro na yule mfuasi mwingine wakaanza kuelekea kwenye kaburi. Wote walikuwa wakikimbia, lakini yule mfuasi mwingine alikimbia kwa kasi zaidi kuliko Petro na kuwasili wa kwanza kaburini. Alipofika akainama chini na kuchungulia ndani ya kaburi. Humo akaviona vipande vya nguo za kitani vikiwa pale chini, lakini hakuingia ndani. Hatimaye Simoni Petro akafika kaburini na kuingia ndani. Naye aliviona vipande vile vya nguo za kitani vikiwa chini mle ndani. Pia aliiona nguo iliyokuwa imezungushwa kichwani kwa Yesu. Hii ilikuwa imekunjwa na kuwekwa upande mwingine tofauti na pale zilipokuwepo nguo za kitani. Kisha mfuasi mwingine, yule aliyefika kwanza kaburini, akaingia ndani. Yeye aliona yaliyotokea na akaamini. (Wafuasi hawa walikuwa bado hawajayaelewa yale Maandiko kwamba Yesu alipaswa kufufuka kutoka wafu.) Kisha wafuasi wakarudi nyumbani. Lakini Mariamu akabaki amesimama nje ya kaburi, akilia. Aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi alipokuwa akilia. Mle ndani akawaona malaika wawili waliovaa nguo nyeupe na wameketi mahali ulipokuwa mwili wa Yesu. Mmoja amekaa sehemu kilipolazwa kichwa na mwingine aliketi sehemu miguu ilipokuwa imewekwa. Malaika wakamwuliza Mariamu, “Mwanamke, kwa nini unalia?” Mariamu akajibu, “Wameuondoa mwili wa Bwana wangu, na sijui wameuweka wapi.” Wakati Mariamu aliposema hivi, akageuka nyuma na kumwona Yesu amesimama pale. Lakini hakujua kuwa huyo alikuwa ni Yesu. Akamwuliza, “Mwanamke, kwa nini unalia? Je, unamtafuta nani?” Yeye alifikiri kuwa huyu alikuwa ni mtunzaji wa bustani. Hivyo akamwambia, “Je, ulimwondoa Bwana? Niambie umemweka wapi. Nami nitaenda kumchukua.” Yesu akamwita, “Mariamu.” Mariamu akamgeukia na kumwambia kwa Kiaramu, “ Raboni ”, (hii ikiwa na maana “Mwalimu”). Yesu akamwambia, “Hupaswi kunishika! Kwani bado sijapaa kwenda huko juu kwa Baba yangu. Lakini nenda ukawaambie wafuasi wangu maneno haya: ‘Ninarudi kwa Baba yangu ambaye pia ni Baba yenu. Ninarudi kwa Mungu wangu ambaye pia ni Mungu wenu.’” Mariamu Magdalena akaenda kwa wafuasi na kuwaambia, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaeleza yale Yesu aliyomwambia. Ilikuwa siku ya Jumapili, na jioni ile wafuasi walikuwa pamoja. Nao walikuwa wamefunga milango kwa kuwa waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Ghafla, Yesu akawa amesimama pale katikati yao. Akasema, “Amani iwe nanyi!” Mara baada ya kusema haya, aliwaonesha mikono yake na ubavu wake. Wafuasi walipomwona Bwana, walifurahi sana. Kisha Yesu akasema tena, “Amani iwe nanyi. Kama vile Baba alivyonituma, nami sasa nawatuma ninyi vivyo hivyo.” Kisha akawapumulia pumzi na kusema, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Mkisamehe dhambi zake mtu yeyote, dhambi zake hizo zitasamehewa. Kama kuna mtu yeyote ambaye hamtamsamehe dhambi zake, dhambi zake huyo hazitasamehewa.” Tomaso (aliyeitwa Pacha) alikuwa ni mmoja wa wale kumi na mbili, lakini hakuwapo pamoja na wafuasi wengine Yesu alipokuja. Wakamwambia, “Tulimwona Bwana.” Tomaso akasema, “Hiyo ni ngumu kuamini. Ninahitaji kuona makovu ya misumari katika mikono yake, niweke vidole vyangu ubavuni. Ndipo tu nitakapoamini.” Juma moja baadaye wafuasi walikuwemo katika nyumba ile tena, na Tomaso alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja na kusimama katikati yao. Akasema, “Amani iwe nanyi!” Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa. Iangalie mikono yangu. Weka mkono wako hapa ubavuni mwangu. Acha kuwa na mashaka na uamini.” Tomaso akamwambia Yesu, “Bwana wangu na Mungu wangu!” Yesu akamwambia, “Unaamini kwa sababu umeniona. Wana baraka nyingi watu wale wanaoniamini bila kuniona!” Yesu alifanya ishara nyingine nyingi za miujiza ambazo wafuasi wake waliziona, na ambazo hazikuandikwa kwenye kitabu hiki. Lakini haya yameandikwa ili muweze kuamini kwamba Yesu ni Masihi, Mwana wa Mungu. Kisha, kwa kuamini, mpate uzima kupitia jina lake. Baadaye, Yesu akawatokea tena wafuasi wake karibu na Ziwa Galilaya. Hivi ndivyo ilivyotokea: Baadhi ya wafuasi wake walikuwa pamoja; Simoni Petro, Tomaso (aliyeitwa Pacha), Nathanaeli kutoka Kana kule Galilaya, wana wawili wa Zebedayo, na wafuasi wengine wawili. Simoni Petro akasema, “Ninaenda kuvua samaki.” Wafuasi wengine wakasema, “Sisi sote tutaenda pamoja nawe.” Hivyo wote wakatoka na kwenda kwenye mashua. Usiku ule walivua lakini hawakupata kitu. Asubuhi na mapema siku iliyofuata Yesu akasimama ufukweni mwa bahari. Hata hivyo wafuasi wake hawakujua kuwa alikuwa ni yeye Yesu. Kisha akawauliza, “Rafiki zangu, mmepata samaki wo wote?” Wao wakajibu, “Hapana.” Yesu akasema, “Tupeni nyavu zenu kwenye maji upande wa kulia wa mashua yenu. Nanyi mtapata samaki huko.” Nao wakafanya hivyo. Wakapata samaki wengi kiasi cha kushindwa kuzivuta nyavu na kuziingiza katika mashua. Mfuasi aliyependwa sana na Yesu akamwambia Petro, “Mtu huyo ni Bwana!” Petro aliposikia akisema kuwa alikuwa Bwana, akajifunga joho lake kiunoni. (Alikuwa amezivua nguo zake kwa vile alitaka kufanya kazi.) Ndipo akaruka majini. Wafuasi wengine wakaenda ufukweni katika mashua. Wakazivuta nyavu zilizojaa samaki. Nao hawakuwa mbali sana na ufukwe, walikuwa kadiri ya mita 100 tu. Walipotoka kwenye mashua na kuingia kwenye maji, wakaona moto wenye makaa yaliokolea sana. Ndani ya moto huo walikuwemo samaki na mikate pia. Kisha Yesu akasema leteni baadhi ya samaki mliowavua. Simoni Petro akaenda kwenye mashua na kuvuta wavu kuelekea ufukweni. Wavu huo ulikuwa umejaa samaki wakubwa, wapatao 153 kwa ujumla! Lakini pamoja na wingi wa samaki hao, nyavu hazikukatika. Yesu akawaambia, “Njooni mle.” Hakuna hata mfuasi mmoja aliyemwuliza, “Wewe ni nani?” Walijua yeye alikuwa ni Bwana. Yesu akatembea ili kuchukua mikate na kuwapa. Akawapa samaki pia. Hii sasa ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wafuasi wake baada ya kufufuka kutoka wafu. Walipomaliza kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, “Simoni, mwana wa Yohana, je, unanipenda kuliko watu wote hawa wanavyonipenda?” Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, unajua kuwa nakupenda.” Kisha Yesu akamwambia, “Wachunge wanakondoo wangu.” Kwa mara nyingine Yesu akamwambia, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?” Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, wewe unajua kuwa nakupenda.” Kisha Yesu akasema, “Watunze kondoo wangu.” Mara ya tatu Yesu akasema, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?” Petro akahuzunika kwa sababu Yesu alimuuliza mara tatu, “Unanipenda?” Akasema, “Bwana, unafahamu kila kitu. Unajua kuwa nakupenda!” Yesu akamwambia, “Walinde kondoo wangu. Ukweli ni huu, wakati ulipokuwa mdogo, ulijifunga mwenyewe mkanda wako kiunoni na kwenda ulikotaka. Lakini utakapozeeka, utainyoosha mikono yako, na mtu mwingine atakufunga mkanda wako. Watakuongoza kwenda mahali usikotaka kwenda.” (Yesu alisema hivi kumwonyesha jinsi Petro atakavyokufa ili kumpa utukufu Mungu.) Kisha akamwambia Petro, “Nifuate!” Petro akageuka na kumwona yule mfuasi mwingine aliyependwa sana na Yesu akitembea nyuma yao. (Huyu alikuwa ni mfuasi aliyejilaza kwa Yesu wakati wa chakula cha jioni na kusema, “Bwana, ni nani atakayekusaliti kwa maadui zako?”) Petro alipomwona nyuma yao, akamwuliza Yesu, “Bwana, vipi kuhusu yeye?” Yesu akajibu, “Labda nataka awe hai hadi nitakaporudi. Hilo wewe usilijali. Wewe nifuate!” Kwa hiyo habari ikaenea miongoni mwa wafuasi wa Yesu. Wao walikuwa wakisema kuwa mfuasi huyo asingekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa asingekufa. Yeye alisema tu, “Labda nataka awe hai hadi nitakaporudi. Hilo wewe usilijali.” Huyo mfuasi ndiye yeye anayesimulia habari hizi. Ndiye ambaye sasa ameziandika habari zote hizi. Nasi tunajua kuwa anayoyasema ni kweli. Kuna mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu. Kama kila moja ya hayo yote yangeandikwa, nafikiri ulimwengu wote usingevitosha vitabu ambavyo vingeandikwa. Mpendwa Theofilo: Katika kitabu cha kwanza niliandika kuhusu kila kitu ambacho Yesu alitenda na kufundisha tangu mwanzo mpaka siku alipochukuliwa juu mbinguni. Kabla hajaondoka, alizungumza na mitume aliowachagua kwa msaada wa Roho Mtakatifu kuhusu mambo waliyotakiwa kufanya. Hii ilikuwa baada ya kifo chake, ambapo aliwathibitishia kwa namna nyingi kuwa alikuwa hai. Mitume walimwona Yesu mara nyingi kwa muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kutoka kwa wafu. Naye Yesu alizungumza nao kuhusu ufalme wa Mungu. Wakati mmoja Yesu alipokuwa akila pamoja nao, aliwaambia wasiondoke Yerusalemu. Aliwaambia, “Kaeni hapa mpaka mtakapopokea kile ambacho Baba aliahidi kutuma. Kumbukeni, niliwaambia juu yake. Yohana aliwabatiza watu kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.” Mitume walipokuwa pamoja, walimwuliza Yesu, “Bwana, huu ni wakati wako wa kuwarudishia Waisraeli ufalme wao tena?” Yesu akawaambia, “Baba peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na nyakati. Si juu yenu kujua. Lakini Roho Mtakatifu atawajia na kuwapa nguvu. Nanyi mtakuwa mashahidi wangu. Mtawahubiri watu kuhusu mimi kila mahali, kuanzia humu Yerusalemu, Uyahudi yote, katika Samaria na hatimaye kila mahali ulimwenguni.” Baada ya kusema haya, alichukuliwa juu mbinguni. Walipokuwa wanaangalia juu angani, wingu lilimficha na hawakuweza kumwona. Walikuwa bado wanatazama angani alipokuwa anakwenda. Ghafla malaika wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama pembeni mwao. Wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, kwa nini mmesimama hapa na mnatazama angani? Mlimwona Yesu akichukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni. Atarudi katika namna hii hii kama mlivyomwona akienda.” Ndipo mitume walirudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, ulio umbali wa kama kilomita moja kutoka Yerusalemu. Walipoingia mjini, walikwenda kwenye chumba cha ghorofani walikokuwa wanakaa. Hawa ndiyo wale waliokuwepo: Petro, Yohana, Yakobo, na Andrea, Filipo, Thomasi, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo (mwana wa Alfayo), na Simoni Mzelote, na Yuda (mwana wa Yakobo). Mitume hawa wote walikuwa pamoja na waliomba kwa nia moja. Baadhi ya wanawake, Mariamu mama wa Yesu na wadogo zake Bwana Yesu walikuwepo pale pamoja na mitume. Baada ya siku chache waamini waliokuwa kama mia moja na ishirini walikutana pamoja. Petro alisimama na kusema, “Kaka na dada zangu, katika Maandiko Roho Mtakatifu alisema kupitia Daudi kwamba jambo fulani lazima litatokea. Alizungumza kuhusu Yuda, yule aliyekuwa katika kundi letu wenyewe. Yuda alihudumu pamoja nasi. Roho alisema Yuda atawaongoza watu kumkamata Yesu.” *** (Kwa kufanya hili Yuda alilipwa pesa. Alinunulia shamba pesa hizo. Lakini aliangukia kichwa chake, mwili wake ukapasuka, na matumbo yake yote yakamwagika nje. Na watu wote wa Yerusalemu wanalijua hili. Ndiyo maana waliliita shamba hilo Akeldama, ambalo maana yake kwa Kiaramu ni “Shamba la Damu”.) Petro akasema, “Katika kitabu cha Zaburi, jambo hili limeandikwa kuhusu Yuda: ‘Watu wasipakaribie mahali pake; Yeyote asiishi hapo.’ Pia imeandikwa kuwa: ‘Mtu mwingine achukue kazi yake.’ Hivyo ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi ili awe shahidi wa ufufuo wa Bwana Yesu. Ni lazima awe mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana Yesu alipokuwa pamoja nasi. Ni lazima awe yule ambaye amekuwa pamoja nasi tangu Yohana alipokuwa anabatiza watu mpaka siku ambayo Bwana Yesu alichukuliwa kutoka kwetu na kwenda mbinguni.” *** Kisha waliwasimamisha watu wawili mbele ya kundi. Mmoja aliitwa Yusufu Barsaba, ambaye pia aliitwa Yusto. Mwingine aliitwa Mathiasi. Wakaomba wakisema, “Bwana unajua mioyo ya watu wote. Tuonyeshe kati ya watu hawa wawili uliyemchagua kufanya kazi hii. Yuda aliiacha na kuifuata njia yake. Bwana tuonyeshe ni nani achukue sehemu yake kama mtume!” *** Kisha wakapiga kura kumchagua mmoja kati ya watu hao wawili. Kura ikaonesha Mathiasi ndiye Bwana anamtaka. Hivyo akawa mtume pamoja na wale wengine kumi na moja. Siku ya Pentekoste ilipofika, wote walikuwa pamoja sehemu moja. Ghafla sauti ikaja kutoka mbinguni. Ilikuwa kama sauti ya upepo mkali unaovuma. Sauti hii ikajaa katika nyumba yote walimokuwa. Waliona miali iliyoonekana kama ndimi za moto. Miali ilitengana na kukaa juu ya kila mmoja wao pale. Wote walijaa Roho Mtakatifu na wakaanza kuzungumza kwa lugha tofauti. Roho Mtakatifu aliwapa uwezo wa kuzungumza lugha hizi. Wakati haya yanatokea, walikuwepo Wayahudi waliorudi makwao. Hawa walikuwa wacha Mungu kutoka kila taifa ulimwenguni waliokuja mjini Yerusalemu. Kundi kubwa lilikusanyika kwa sababu walisikia kelele. Walishangaa kwa sababu, mitume walipokuwa wakitamka maneno kila mtu alisikia kwa lugha ya kwao. Watu wote walilishangaa hili. Hawakuelewa ni kwa namna gani mitume waliweza kufanya hili. Wakaulizana, “Tazama! Watu wote hawa tunaowasikia wanatoka Galilaya. Lakini tunawasikia wanatamka maneno kwa lugha zetu za asili. Hili linawezekanaje? Sisi tunatoka sehemu hizo mbalimbali: Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto, Asia, Frigia, Pamfilia, Misri na maeneo ya Libya karibu na mji wa Kirene, Rumi, Krete na Uarabuni. Baadhi yetu ni Wayahudi kwa kuzaliwa na wengine si Wayahudi, bali wamechagua kumwabudu Mungu kama Wayahudi. Tunatoka katika nchi hizi mbalimbali, lakini tunawasikia watu hawa wakizungumza kwa lugha zetu tofauti! Sisi sote tunaweza kuelewa yote wanayosema kuhusu matendo makuu ya Mungu.” Watu wote walistaajabu na pia walichanganyikiwa. Wakaulizana, “Hii yote inamaanisha nini?” Lakini wengine waliwacheka mitume, wakisema wamelewa kwa mvinyo mwingi waliokunywa. Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini. Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika: ‘Mungu anasema: Katika siku za mwisho, nitaimimina Roho yangu kwa watu wote. Wana wenu na binti zenu watatabiri. Vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Katika siku hizo nitaimimina Roho yangu kwa watumishi wangu, wanaume na wanawake, nao watatabiri. Nitafanya maajabu juu angani. Nitasababisha ishara chini duniani. Kutakuwa damu, moto na moshi mzito. Jua litakuwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja. Na kila amwombaye Bwana’ ataokolewa. Ndugu zangu Waisraeli, sikilizeni ninayowaambia: Mungu aliwaonesha wazi kuwa Yesu kutoka Nazareti alikuwa mtu wake. Mungu alilithibitisha hili kwa miujiza, maajabu na ishara alizotenda Yesu. Ninyi nyote mliyaona mambo haya, na mnajua hii ni kweli. Yesu aliletwa kwenu, nanyi mkamwua. Kwa kusaidiwa na watu wasioijali sheria yetu, mlimpigilia msalabani. Lakini Mungu alijua hili lingetokea. Ulikuwa mpango wake, mpango alioutengeneza tangu mwanzo. Yesu aliteseka kwa maumivu makali ya kifo, lakini Mungu alimweka huru. Akamfufua kutoka kwa wafu. Mauti ilishindwa kumshikilia. Daudi alilisema hili kuhusu Yesu: ‘Sijasahau kuwa Bwana yu pamoja nami. Yupo hapa pembeni yangu, hivyo hakuna kinachoweza kunidhuru. Ndiyo sababu ninafurahi sana, na ninaimba kwa furaha! Lipo tumaini hata kwa ajili ya mwili wangu huu dhaifu, kwa sababu wewe Bwana hutaniacha kaburini. Hautauacha mwili wa mtumishi wako mwaminifu kuozea huko. Umenionyesha njia iendayo uzimani. Kuwa pamoja nawe kutanijaza furaha.’ Ndugu zangu, ninaweza kuwaambia kwa ujasiri kuhusu Daudi, baba yetu mkuu. Alikufa, akazikwa, na kaburi lake liko hapa pamoja nasi hata leo. Alikuwa nabii na alijua kitu ambacho Mungu alisema. Mungu alimwahidi Daudi kwa kuweka Agano kuwa mzaliwa katika familia yake mwenyewe ataketi kwenye kiti cha enzi cha Daudi kama mfalme. Daudi aliliona hili kabla halijatokea. Ndiyo maana alisema hivi kuhusu mfalme ajaye: ‘Hakuachwa kaburini. Mwili wake haukuozea humo.’ Daudi alizungumza kuhusu Masihi kufufuka kutoka kwa wafu. Yesu ndiye ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi sote ni mashahidi wa jambo hili. Tulimwona. Yesu alichukuliwa juu mbinguni. Na sasa ameketi upande wa kulia wa Mungu. Baba amempa Roho Mtakatifu, kama alivyoahidi. Hivyo Yesu amemimina huyo Roho Mtakatifu na hiki ndicho mnachoona na kusikia Daudi hakuchukuliwa mpaka mbinguni. Daudi mwenyewe alisema, ‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kuume hadi nitakapowaweka maadui zako chini ya udhibiti wako.’ Hivyo, watu wote wa Israeli wanapaswa kulijua hili bila kuwa na mashaka: Mungu amemfanya Yesu kuwa Bwana na Masihi. Ndiye yule mliyempigilia msalabani!” Watu waliposikia hili wakahuzunika sana. Wakawauliza Petro na mitume wengine, “Ndugu zetu, tufanye nini?” Petro akawaambia, “Geuzeni mioyo na maisha yenu na kila mmoja wenu abatizwe katika jina la Yesu Kristo. Ndipo Mungu atawasamehe dhambi zenu, na mtapokea zawadi ya Roho Mtakatifu. Ahadi hii ni kwa ajili yenu ninyi, watoto wenu na vizazi vijavyo. Ni kwa kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu anamwita kwake mwenyewe.” Petro aliwaonya kwa maneno mengine mengi; aliwasihi, akawaambia, “Jiokoeni na uovu unaofanywa na watu wanaoishi sasa!” Ndipo wale walioyakubali yale aliyosema Petro wakabatizwa. Yapata watu elfu tatu waliongezwa kwenye kundi la waamini siku ile. Waamini walitumia muda wao kusikiliza mafundisho ya mitume. Walishirikiana kila kitu kwa pamoja. Walikula na kuomba pamoja. Maajabu mengi na ishara nyingi zilikuwa zinatokea kupitia mitume, na hivyo kila mtu aliingiwa na hofu na akamtukuza Mungu. Waamini wote walikaa pamoja, na kushirikiana kila kitu. Waliuza mashamba yao na vitu walivyomiliki, kisha wakatoa fedha na kuwapa wenye kuhitaji. Waamini waliendelea kukutana pamoja katika eneo la Hekalu. Pia walikula pamoja katika nyumba zao. Walikuwa na furaha kushirikiana chakula chao na walikula kwa mioyo mikunjufu. Waamini walimsifu Mungu na waliheshimiwa na watu wote. Watu wengi zaidi waliokolewa kila siku, na Bwana alikuwa akiwaongeza kwenye kundi lao. Siku moja Petro na Yohana walikwenda eneo la Hekalu saa tisa mchana, muda wa kusali na kuomba Hekaluni kama ilivyokuwa desturi. Walipokuwa wanaingia katika eneo la Hekalu, mtu aliyekuwa mlemavu wa miguu maisha yake yote alikuwa amebebwa na baadhi ya rafiki zake waliokuwa wanamleta Hekaluni kila siku. Walimweka pembezoni mwa mojawapo ya Malango nje ya Hekalu. Lango hilo liliitwa Lango Zuri. Na mtu huyo alikuwa akiwaomba pesa watu waliokuwa wanaingia Hekaluni. Siku hiyo alipowaona Petro na Yohana wakiingia eneo la Hekalu, aliwaomba pesa. Petro na Yohana, walimtazama mtu huyo, wakamwambia, “Tutazame!” Akawatazama akitumaini kuwa wangempa pesa. Lakini Petro akasema, “Sina fedha wala dhahabu yoyote, lakini nina kitu kingine ninachoweza kukupa. Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti simama na utembee!” Kisha Petro akamshika mkono wake wa kulia, akamnyenyua na kumsimamisha. Ndipo nyayo na vifundo vyake vikatiwa nguvu papo hapo. Akaruka juu, akasimama kwa miguu yake na akaanza kutembea. Akaingia ndani ya eneo la Hekalu pamoja nao huku akitembea na kurukaruka akimsifu Mungu. Watu wote walimtambua. Walimjua kuwa ni mlemavu wa miguu ambaye mara nyingi huketi kwenye Lango Zuri la Hekalu akiomba pesa. Lakini sasa walimwona anatembea na kumsifu Mungu. Walishangaa na hawakuelewa hili limewezekanaje. *** Huku wakishangaa, watu wale waliwakimbilia Petro na Yohana pale walikokuwa katika Ukumbi wa Sulemani. Mtu yule aliyeponywa alikuwa akingali amewang'anga'nia Petro na Yohana. Petro alipoona hili, aliwaambia watu: “Ndugu zangu Wayahudi, kwa nini mnashangaa hili? Mnatutazama kama vile ni kwa nguvu zetu tumemfanya mtu huyu atembee. Mnadhani hili limetendeka kwa sababu sisi ni wema? Hapana, Mungu ndiye aliyetenda hili! Ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Ni Mungu aliyeabudiwa na baba zetu wote. Kwa kufanya hili, alimtukuza Yesu mtumishi wake, yule ambaye ninyi mlimtoa ili auawe. Pilato alipotaka kumwachia huru, mlimwambia Pilato kuwa hamumtaki Yesu. Yesu alikuwa Mtakatifu na mwema, lakini mlimkataa na badala yake mlimwambia Pilato amwache huru mwuaji na awape ninyi. Na hivyo mlimwua yule awapaye uzima! Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi ni mashahidi wa jambo hili kwani tuliliona kwa macho yetu wenyewe. Huyu mlemavu wa miguu ameponywa kwa sababu tunalo tumaini katika Yesu. Nguvu ya Yesu ndiyo iliyomponya. Mnamwona na mnamfahamu mtu huyu. Ameponywa kabisa kwa sababu ya imani inayotokana na Yesu. Ninyi nyote mmeona hili likitokea! Kaka zangu, ninajua kwamba hamkujua mlilomtendea Yesu wakati ule. Hata viongozi wenu hawakujua walilokuwa wanatenda. Lakini Mungu alikwishasema kupitia manabii kuwa mambo haya yangetokea. Masihi wake angeteseka na kufa. Nimewaambia jinsi ambavyo Mungu alifanya jambo hili likatokea. Hivyo lazima mbadili mioyo na maisha yenu. Mrudieni Mungu, naye atawasamehe dhambi zenu. Kisha Bwana atawapa muda wa faraja kutokana na masumbufu yenu. Atamtuma Yesu kwenu, aliyemchagua kuwa Masihi wenu. Lakini Yesu lazima akae mbinguni mpaka wakati ambapo kila kitu kitafanywa upya tena. Mungu alikwisha sema kuhusu wakati huu tangu zamani kupitia manabii wake watakatifu. Musa alisema, ‘Bwana Mungu wako atakupa nabii. Nabii huyo atatoka miongoni mwa watu wako. Atakuwa kama mimi. Ni lazima mtii kila kitu atakachowaambia. Na yeyote atakayekataa kumtii nabii huyo atakufa na kutengwa na watu wa Mungu.’ Samweli, na manabii wengine wote walisema kwa niaba ya Mungu. Baada ya Samweli, walisema kuwa wakati huu ungekuja. Na kile ambacho manabii walikisema ni kwa ajili yenu ninyi wazaliwa wao. Mmepokea Agano ambalo Mungu alilifanya na baba zenu. Mungu alimwambia baba yenu Ibrahimu kuwa, ‘Kila taifa duniani litabarikiwa kupitia wazaliwa wako.’ Mungu amemtuma Yesu, mtumishi wake maalumu. Alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kuwageuza kila mmoja wenu aache njia zake za uovu.” Petro na Yohana walipokuwa wanazungumza na watu, ghafla baadhi ya viongozi wa Kiyahudi waliwaendea. Walikuwepo baadhi ya makuhani, mkuu wa askari wanaolinda Hekalu na baadhi ya Masadukayo. Walikasirika kwa sababu ya mafundisho ambayo Petro na Yohana walikuwa wanawafundisha na kuwaambia watu kuhusu Yesu. Mitume walikuwa wanafundisha pia kwamba watu watafufuka kutoka kwa wafu. Waliwakamata Petro na Yohana. Kwa kuwa ilikuwa jioni tayari, waliwaweka gerezani usiku ule mpaka siku iliyofuata. Lakini watu wengi waliowasikia mitume waliamini walichosema. Na siku hiyo idadi ya watu katika kundi la waamini ikafikia watu 5,000. Siku iliyofuata, watawala wa Kiyahudi, wazee na walimu wa sheria walikutana Yerusalemu. Kuhani mkuu Anasi alikuwepo. Kayafa, Yohana, Iskanda na jamaa wengine wa kuhani mkuu walikuwepo pia. Waliwasimamisha Petro na Yohana mbele ya watu wote. Wakawauliza maswali mengi, “Mliwezaje kumponya mlemavu wa miguu huyu? Mlitumia nguvu gani? Mmefanya hili kwa mamlaka ya nani?” Ndipo Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akawaambia, “Enyi watawala nanyi wazee wa watu, mnatuuliza leo ni nini tulifanya kumsaidia huyu mlemavu wa miguu? Mnatuuliza nini kilimponya? Tunataka ninyi nyote na watu wote wa Israeli mtambue kuwa mtu huyu aliponywa na nguvu ya Yesu Kristo kutoka Nazareti. Mlimpigilia Yesu msalabani, lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Mtu huyu alikuwa mlemavu wa miguu, lakini sasa ni mzima. Anaweza kusimama hapa mbele zenu kwa sababu ya nguvu ya Yesu! Yesu ndiye ‘Jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa. Lakini jiwe hili limekuwa jiwe na msingi.’ Yesu peke yake ndiye anayeweza kuokoa watu. Jina lake ndiyo nguvu pekee iliyotolewa kumwokoa mtu yeyote ulimwenguni. Ni lazima tuokoke kupitia yeye!” Viongozi wa Kiyahudi walijua kuwa Petro na Yohana walikuwa watu wa kawaida wasio na elimu yo yote. Lakini walikuwa wanazungumza kwa ujasiri bila woga; viongozi walishangaa. Walitambua pia kuwa Petro na Yohana walikuwa pamoja na Yesu. Walimwona aliyeponywa akiwa amesimama kwa miguu yake mwenyewe pembeni mwa mitume. Na hivyo walishindwa kuzungumza chochote kilicho kinyume na mitume. Viongozi wa Kiyahudi wakawaambia mitume watoke nje ya chumba cha mkutano wa baraza. Kisha viongozi wakajadiliana wao wenyewe juu ya nini wanachopaswa kufanya. Wakaulizana, “Tuwafanye nini watu hawa? Kila mtu katika Yerusalemu anajua kuhusu muujiza walioufanya kama ishara kutoka kwa Mungu. Ni dhahiri, hatuwezi kusema muujiza huo haukufanyika. Lakini ni lazima tuwatishe ili wasiendelee kuwaambia watu kutumia jina lile. Ili tatizo hili lisisambae miongoni mwa watu.” Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakawaita Petro na Yohana ndani tena. Wakawaambia wasiseme wala kufundisha kitu chochote kwa kutumia jina la Yesu. Lakini Petro na Yohana wakawajibu, “Mnadhani kipi ni sahihi? Mungu angetaka nini? Je, tunapaswa kuwatii ninyi au tumtii Mungu? Hatuwezi kukaa kimya. Ni lazima tuwaambie watu kuhusu yale tuliyoona na kusikia.” Viongozi wa Kiyahudi hawakupata sababu za kuwaadhibu mitume, kwa sababu watu wote walikuwa wanamsifu Mungu kwa kile kilichotendeka. Muujiza huu ulikuwa ishara kutoka kwa Mungu. Mtu aliyeponywa alikuwa na miaka zaidi ya arobaini. Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakawaonya mitume tena na kuwaacha waende wakiwa huru. *** Petro na Yohana waliondoka kwenye mkutano wa viongozi wa Kiyahudi na kurudi kwa waamini wenzao. Wakalieleza kundi la waamini kila kitu walichoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. Waamini waliposikia hili, wote kwa pamoja wakamwomba Mungu wakiwa na nia moja. Wakasema, “Bwana wa wote, wewe ndiye uliyeumba mbingu, dunia, bahari na kila kitu ulimwenguni. Baba yetu Daudi alikuwa mtumishi wako. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu aliandika maneno haya: ‘Kwa nini mataifa yanatenda kwa kiburi? Kwa nini watu wanapanga mipango isiyofaa kama hii? Wafalme wa dunia hujiandaa kwa mapigano, na watawala hukusanyika pamoja kinyume na Bwana na kinyume na Masihi wake.’ Ndicho hasa kilichotokea wakati Herode, Pontio Pilato, mataifa mengine na watu wa Israeli walipokusanyika pamoja hapa Yerusalemu wakawa kinyume na Yesu; Masihi, Mtumishi wako mtakatifu. Watu hawa waliokusanyika pamoja kinyume na Yesu waliwezesha mpango wako kukamilika. Ilifanyika kwa sababu ya nguvu zako na matakwa yako. Na sasa, Bwana, sikiliza wanayosema. Wanajaribu kututisha. Sisi ni watumishi wako. Tusaidie ili tuseme yale unayotaka tuseme bila kuogopa. Tusaidie, ili tuwe jasiri kwa kutuonesha nguvu zako. Ponya Wagonjwa. Fanya ishara na maajabu kutokea kwa mamlaka ya Yesu mtumishi wako mtakatifu.” Baada ya waamini kuomba, mahali walipokuwa palitikisika. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, na wakaendelea kuhubiri Habari Njema bila woga. Kundi lote la waamini waliungana katika kuwaza na katika mahitaji yao. Hakuna aliyesema vitu alivyokuwa navyo ni vyake peke yake. Badala yake walishirikiana kila kitu. Kwa nguvu kuu mitume walifanya ijulikane kwa kila mmoja kwamba Bwana Yesu alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na Mungu aliwabariki sana waamini wote. Hakuna aliyepungukiwa kitu. Kila aliyemiliki shamba au nyumba aliuza na kuleta pesa alizopata, na kuzikabidhi kwa mitume. Kisha kila mtu akapewa kiasi alichohitaji. Mmoja wa waamini aliitwa Yusufu. Mitume walimwita Barnaba, jina linalomaanisha “Mtu anayewatia moyo wengine.” Alikuwa Mlawi mzaliwa wa Kipro. Yusufu aliuza shamba alilomiliki. Akaleta pesa na kuwapa mitume. Alikuwepo mtu aliyeitwa Anania na mke wake aliyeitwa Safira. Anania aliuza shamba lake, lakini aliwapa mitume sehemu tu ya pesa alizopata baada ya kuuza shamba lake. Kwa siri alibakiza kiasi cha pesa kwa ajili yake mwenyewe. Mke wake alilijua hili na akalikubali. Petro akasema, “Anania, kwa nini umemruhusu Shetani aitawale akili yako kwa wazo la namna hii? Umebakiza sehemu ya pesa kwa ajili yako mwenyewe na kumdanganya Roho Mtakatifu! Je, kabla ya kuuza shamba, halikuwa lako? Na hata baada ya kuliuza, ungeweza kutumia pesa kwa namna yoyote unayotaka. Imekuwaje hata ufikirie kufanya jambo hili? Hukutudanganya sisi bali Mungu!” Anania aliposikia hili, alianguka chini na kufa. Baadhi ya vijana wakaja na kuufunga mwili wake. Wakautoa nje na kuuzika. Kila mtu aliyelisikia hili aliingiwa hofu. *** Baada ya kama saa tatu baadaye, mkewe naye alifika. Safira hakujua kilichompata mumewe. Petro akamwambia, “Niambie mlipata pesa kiasi gani baada ya kuuza shamba lenu. Kilikuwa kiasi hiki?” Safira akajibu, “Ndiyo, hicho ndicho tulichopata baada ya kuuza shamba.” Petro akamwambia, “Kwa nini wewe na mume wako mlikubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Sikiliza! Unasikia vishindo hivyo vya miguu? Watu waliomzika mume wako, wako mlangoni. Watakuchukua nje kwa njia hiyo hiyo.” Safira akaanguka miguuni kwa Petro na kufa papo hapo. Vijana wakaingia, walipomwona amekwisha kufa, walimchukua na kumzika kando ya mume wake. Kanisa lote na watu wote waliosikia kuhusu hili waliingiwa hofu. Mitume walipewa nguvu ya kufanya ishara nyingi za miujiza na maajabu katikati ya watu. Walikuwa wanakutanika pamoja mara kwa mara katika eneo la Hekalu lililoitwa Ukumbi wa Sulemani. Hakuna mtu yeyote ambaye hakuwa mwamini alikaa na kushirikiana nao, lakini kila mtu alisema mambo mazuri juu yao. Watu wengi zaidi na zaidi walimwamini Bwana; na watu wengi, wanaume kwa wanawake waliongezwa katika kundi la waamini. Hivyo watu waliwatoa wagonjwa majumbani na kuwaweka mitaani katika vitanda vidogo na mikeka. Walitumaini kuwa ikiwa Petro atapita karibu yao na kivuli chake kikawaangukia watapona. Watu walikuja kutoka katika miji kuzunguka Yerusalemu. Waliwaleta wagonjwa au waliosumbuliwa na pepo wachafu. Wote waliponywa. Kuhani mkuu na wafuasi wake wote wa karibu, kundi liitwalo Masadukayo wakaingiwa wivu sana. Waliwakamata mitume na kuwafunga katika gereza la mji. Lakini wakati wa usiku, malaika wa Bwana alifungua milango ya gereza. Malaika akawaongoza mitume nje ya gereza na kusema, “Nendeni mkasimame katika eneo la Hekalu. Waelezeni watu kila kitu kuhusu maisha haya mapya.” Mitume waliposikia hili, walifanya kama walivyoambiwa. Walikwenda katika eneo la Hekalu asubuhi na mapema jua lilipokuwa linachomoza na kuanza kuwafundisha watu. Kuhani mkuu na wafuasi wake wakakusanyika na kuitisha mkutano wa Baraza kuu na wazee wa Kiyahudi. Wakawatuma baadhi ya watu gerezani ili wawalete mitume kwao. Watu wale walipokwenda gerezani, hawakuwaona mitume. Hivyo walirudi na kuwaambia viongozi wa Kiyahudi kuhusu hili. Walisema, “Gereza lilikuwa limefungwa na milango ilikuwa imefungwa. Walinzi walikuwa wamesimama milangoni. Lakini tulipofungua milango, gereza lilikuwa tupu!” Mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani walipolisikia hili, walichanganyikiwa na kujiuliza maana yake ni nini. Ndipo mtu mwingine akaja na kuwaambia, “Sikilizeni! Watu mliowafunga gerezani wamesimama katika eneo la Hekalu wanawafundisha watu!” Mkuu wa walinzi na askari walinzi wa Hekalu walikwenda na kuwarudisha mitume. Lakini askari hawakutumia nguvu, kwa sababu waliwaogopa watu. Waliogopa watu wangewapiga kwa mawe mpaka wafe. Askari waliwaleta mitume na kuwasimamisha mbele ya baraza. Kuhani mkuu akawauliza. Akisema, “Tuliwaambia msifundishe tena kwa kutumia jina lile. Lakini tazameni mlichofanya! Mmeujaza mji wa Yerusalemu kwa mafundisho yenu. Na mnajaribu kutulaumu sisi kwa sababu ya kifo chake.” Petro na mitume wengine wakajibu, “Ni lazima tumtii Mungu, siyo wanadamu! Mlimwua Yesu kwa kumpigilia msalabani. Lakini Mungu, Mungu yule yule wa Baba zetu, alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Yesu ndiye ambaye Mungu amemtukuza kwa kumpa nafasi upande wake wa kuume. Amemfanya kuwa Kiongozi na Mwokozi wetu. Mungu alifanya hivi ili kuwapa watu wote wa Israeli fursa ya kubadilika na kumgeukia Mungu ili dhambi zao zisamehewe. Tuliona mambo haya yote yakitokea, na tunathibitisha kuwa ni ya kweli. Pia, Roho Mtakatifu anaonesha kuwa mambo haya ni ya kweli. Mungu amemtoa Roho huyu kwa ajili ya wote wanaomtii Yeye.” Wajumbe wa Baraza waliposikia haya, walikasirika sana. Walianza kupanga namna ya kuwaua mitume. Lakini mjumbe mmoja wa Baraza, Farisayo aliyeitwa Gamalieli, akasimama, alikuwa mwalimu wa sheria na watu wote walimheshimu. Aliwaambia wajumbe wawatoe nje mitume kwa dakika chache. Kisha akawaambia, “Wanaume wa Israeli, iweni waangalifu kwa kile mnachopanga kuwatendea watu hawa. Mnakumbuka Theuda alipotokea? Alijidai kuwa alikuwa mtu mkuu, na wanaume kama mia nne waliungana naye. Lakini aliuawa na wote waliomfuata walitawanyika. Baadaye, wakati wa sensa, mtu mmoja aitwaye Yuda alikuja kutoka Galilaya. Watu wengi walijiunga kwenye kundi lake, lakini yeye pia aliuawa na wafuasi wake wote walitawanyika. Na sasa ninawaambia, kaeni mbali na watu hawa. Waacheni. Ikiwa mpango wao ni kitu walichopanga wao wenyewe, utashindwa. Lakini ikiwa ni mpango wa Mungu, hamtaweza kuwazuia. Mnaweza kuwa mnapigana kinyume na Mungu mwenyewe!” Viongozi wa Kiyahudi wakakubaliana na kile alichosema Gamalieli. Wakawaita mitume ndani tena. Wakawachapa viboko na kuwakanya waache kusema na watu kwa kutumia jina la Yesu. Kisha wakawaachia huru. Mitume waliondoka kwenye mkutano wa Baraza, wakifurahi kwamba wamepewa heshima ya kudharauliwa kwa ajili ya Yesu. Mitume hawakuacha kuwafundisha watu. Waliendelea kuzisema Habari Njema, kwamba Yesu ni Masihi. Walifanya hivi kila siku katika eneo la Hekalu na katika nyumba za watu. Watu wengi zaidi walipokuwa wafuasi wa Yesu. Wafuasi waliokuwa wakizungumza Kiyunani walianza kuwalalamikia wafuasi wenzao waliokuwa wanazungumza Kiebrania au Kiaramu. Walisema kuwa wajane wao walikuwa hawapewi mgao wao kutokana na kile wafuasi walikuwa wanapewa kila siku. Mitume kumi na mbili wakaita kundi lote la wafuasi pamoja. Mitume wakawaambia, “Haitakuwa sahihi sisi kuacha kazi yetu ya kuwafundisha watu neno la Mungu ili tuwe wasimamizi wa ugawaji wa chakula kwa watu. Hivyo, kaka zetu na dada zetu, chagueni wanaume saba miongoni mwenu wenye ushuhuda mzuri, watu waliojaa hekima na Roho. Nasi tutawaweka kuwa wasimamizi wa kazi hii muhimu. Na hivyo itatuwezesha sisi kutumia muda wetu wote katika kuomba na kufundisha neno la Mungu.” Kundi lote la waamini likakubaliana na wazo hili. Hivyo wakawachagua wanaume saba: Stefano (aliyejaa imani na Roho Mtakatifu), Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena, na Nikolasi (mtu wa Antiokia aliyeongoka na kufuata dini ya Kiyahudi). Kisha, wakawaweka watu hawa mbele ya mitume, nao mitume waliwaombea na kuweka mikono juu yao. Neno la Mungu lilikuwa linawafikia watu wengi zaidi. Kundi la wafuasi katika Yerusalemu likawa kubwa sana. Hata idadi kubwa ya makuhani wa Kiyahudi waliamini na kutii. Mungu alimpa Stefano nguvu ya kutenda maajabu makuu na miujiza katikati ya watu. Lakini baadhi ya Wayahudi pale waliotoka katika sinagogi la Watu Huru, kama lilivyoitwa. Kundi hili lilijumuisha Wayahudi kutoka Kirene, Iskanderia, Kilikia na Asia. Walianza kubishana na Stefano. Lakini Roho Mtakatifu alimwezesha kuzungumza kwa hekima. Maneno yake yalikuwa na nguvu hata Wayahudi hawa hawakuweza kubishana naye. Hivyo wakawaambia baadhi ya watu waseme, “Tumemsikia Stefano akimtukana Musa na Mungu!” Jambo hili liliwakasirisha sana watu, wazee wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Wakamkamata Stefano na kumpeleka mbele ya Baraza Kuu. Wayahudi wakawaleta baadhi ya watu kwenye mkutano ili kusema uongo kuhusu Stefano. Watu hawa walisema, “Daima mtu huyu husema maneno kinyume na mahali hapa patakatifu na kinyume na Sheria ya Musa. Tulimsikia akisema kwamba Yesu kutoka Nazareti atapaharibu mahali hapa na kubadilisha yale ambayo Musa aliyotuambia kufanya.” Kila mtu aliyekuwa kwenye mkutano wa baraza alikuwa akimshangaa Stefano kwani uso wake ulionekana kama uso wa malaika. Kuhani mkuu akamwambia Stefano, “Mambo haya ndivyo yalivyo?” Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu Wayahudi, nisikilizeni! Mungu wetu mkuu na mwenye utukufu alimtokea Ibrahimu, baba yetu, alipokuwa Mesopotamia. Kabla hajahamia Harani. Mungu alimwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na watu wako, kisha uende katika nchi nitakayokuonesha.’ Hivyo Ibrahimu akaondoka katika nchi ya Ukaldayo na kwenda kuishi Harani. Baada ya baba yake kufa, Mungu akamleta katika nchi hii, mahali mnapoishi sasa. Lakini Mungu hakumpa Ibrahimu sehemu yoyote ya ardhi hii, hata eneo dogo lenye ukubwa wa unyayo wake. Lakini Mungu aliahidi kuwa atampa Ibrahimu nchi hii yeye na watoto wake hapo baadaye. Hii ilikuwa kabla Ibrahimu hajapata watoto. Mungu alimwambia: ‘Wazao wako wataishi katika nchi nyingine. Watakuwa wageni. Watu wa huku watawafanya kuwa watumwa na kuwatendea vibaya kwa miaka mia nne. Lakini nitaliadhibu taifa lililowafanya watumwa.’ Pia, Mungu alisema, ‘Baada ya mambo hayo kutokea, watu wako watatoka katika nchi hiyo. Kisha wataniabudu mahali hapa.’ Mungu aliweka agano na Ibrahimu; alama ya agano hili ilikuwa tohara. Na Ibrahimu alipopata mwana, alimtahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa. Jina la mwanaye lilikuwa Isaka. Pia, Isaka alimtahiri mwanaye Yakobo. Na Yakobo alifanya vivyo hivyo kwa wanaye, ambao ndiyo baba wakuu kumi na mbili wa watu wetu. Baba zetu hawa walimwonea wivu Yusufu ndugu yao na wakamwuza ili awe mtumwa Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, akamwokoa kutoka katika matatizo yake yote. Wakati huo Farao alikuwa mfalme wa Misri. Alimpenda na akamheshimu Yusufu kwa sababu ya hekima ambayo Mungu alimpa. Farao alimfanya Yusufu kuwa gavana wa Misri na msimamizi wa watu wote na kila kitu katika kasri lake. Lakini nchi yote ya Misri na Kanaani zikakosa mvua na mazao ya chakula hayakuweza kuota. Watu waliteseka sana na watu wetu hawakuweza kupata chakula chochote. Lakini Yakobo aliposikia kulikuwa chakula Misri aliwatuma mababa zetu huko. Hii ilikuwa safari yao ya kwanza kwenda Misri. Kisha walikwenda safari ya pili. Safari hii Yusufu akawaeleza ndugu zake yeye ni nani. Ndipo Farao akatambua kuhusu familia ya Yusufu. Kisha Yusufu aliwatuma kaka zake wamwambie Yakobo, baba yake, ahamie Misri. Aliwaalika pia ndugu zake wote, jumla yao wote walikuwa watu sabini na tano. Hivyo Yakobo alitelemka kwenda Misri. Yeye na baba zetu waliishi huko mpaka walipokufa. Baadaye, miili yao ilihamishiwa Shekemu, ambako iliwekwa katika kaburi ambalo Ibrahimu alilinunua kwa fedha kutoka kwa wana wa Hamori. Watu wetu walipokuwa Misri idadi yao iliongezeka. Watu wetu walikuwa wengi mno huko. Ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa Ibrahimu ilikuwa karibu kutimia. Ndipo mfalme mwingine akaanza kutawala Misri, ambaye hakujua lolote kuhusu Yusufu. Mfalme huyu aliwahadaa watu wetu. Akawatendea vibaya sana, akawalazimisha wawaache watoto wao nje ili wafe. Huu ni wakati ambapo Musa alizaliwa. Alikuwa mtoto mzuri sana, na kwa miezi mitatu wazazi wake walimtunza nyumbani. Walipolazimishwa kumtoa nje, Binti wa Farao alimchukua. Alimkuza kama mwanaye wa kumzaa. Musa alielimishwa kwa elimu bora ya Kimisri. Wamisri walimfundisha kila kitu walichojua. Alikuwa mwenye nguvu katika yote aliyosema na kutenda. Musa alipokuwa na umri wa miaka kama arobaini, aliamua kuwatembelea watu wake mwenyewe, watu wa Israeli. Aliona mmoja wao ananyanyaswa na Mmisri, hivyo akamtetea; Musa akampiga na kumwua Mmisri ili kulipiza kwa kumwumiza Mwisraeli. Musa alidhani kwamba watu wake wangeelewa kuwa Mungu alikuwa anamtumia kuwaokoa. Lakini hawakuelewa. Siku iliyofuata, Musa akawaona wawili wa watu wake wakipigana. Alijaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Ninyi ni ndugu! Kwa nini mnataka kuumizana?’ Aliyekuwa akimwumiza mwenzake akamsukuma Musa na akamwambia, ‘Nani amekufanya wewe uwe mtawala na mwamuzi wetu? Unataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri jana?’ Musa alipomsikia akisema hili, alikimbia Misri. Alikwenda kuishi Midiani kama mgeni. Katika kipindi alichoishi huko, alipata wana wawili. Miaka arobaini baadaye, Musa alipokuwa jangwani karibu na Mlima Sinai, malaika alimtokea katika mwali wa moto uliokuwa unawaka katika kichaka. Musa alipoliona hili, alishangaa. Alisogea ili kuangalia kwa karibu. Akasikia sauti; ilikuwa sauti ya Bwana. Bwana alisema, ‘Mimi ni Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zako. Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’ Musa akaanza kutetemeka kwa woga. Aliogopa kukitazama kichaka. Kisha Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako, kwa sababu mahali uliposimama ni ardhi takatifu. Nimewaona watu wangu wanavyoteseka sana Misri. Nimesikia watu wangu wakilia na nimeshuka ili kuwaokoa. Njoo sasa, Musa, ninakutuma urudi Misri.’ Huyu ni Musa ndiye aliyekataliwa na watu wake. Walisema, ‘Nani amekufanya uwe mtawala na mwamuzi wetu?’ Lakini ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mtawala na mwokozi. Mungu alimtuma pamoja na msaada wa malaika, ambaye Musa alimwona katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. Hivyo Musa aliwaongoza watu kutoka Misri. Alitenda maajabu na ishara za miujiza Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa miaka arobaini. Huyu ni Musa yule yule aliyewaambia maneno haya watu wa Israeli: ‘Mungu atakupa nabii. Nabii huyo atakuja kutoka miongoni mwa watu wako mwenyewe. Atakuwa kama mimi.’ Musa huyo huyo alikuwa pamoja na kusanyiko la watu wa Mungu jangwani. Alikuwa na malaika aliyezungumza naye alipokuwa Mlima Sinai, na alikuwa pamoja na baba zetu. Alipokea maneno yaletayo uzima kutoka kwa Mungu, na Musa akatupa sisi Maneno hayo. Lakini baba zetu hawakutaka kumtii Musa. Walimkataa, wakataka kurudi Misri. Walimwambia Haruni, ‘Musa alituongoza kutoka katika nchi ya Misri. Lakini hatujui kilichompata. Hivyo tengeneza miungu ili iwe mbele yetu ituongoze.’ Hivyo watu wakatengeneza kinyago kinachofanana na ndama. Kisha wakakitolea sadaka za kuteketezwa. Walifurahia kile walichotengeneza kwa mikono yao wenyewe. Lakini Mungu akawaacha, nao wakaendelea kuabudu nyota na sayari. Kitabu cha manabii kinasema hivi: ‘Watu wa Israeli, hamkunipa dhabihu jangwani kwa miaka arobaini. Mlibeba hema kwa ajili ya kumwabudia Moleki, na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani. Hizi zilikuwa sanamu mlizotengeneza ili mziabudu. Hivyo nitawahamishia mbali, kuvuka Babeli.’ Baba zetu walikuwa na Hema Takatifu walipokuwa jangwani. Mungu alimwelekeza Musa jinsi ya kutengeneza hema hii. Aliitengeneza kwa kufuata ramani aliyoonyeshwa na Mungu. Baadaye, Yoshua aliwaongoza baba zetu kuteka ardhi ya mataifa mengine. Watu wetu waliingia, na Mungu akawafukuza watu wengine. Watu wetu walipoingia katika ardhi hii mpya, waliibeba hema hii pamoja nao. Watu wetu waliipata hema hii kutoka kwa baba zao, na watu wetu waliitunza mpaka wakati wa Daudi. Mungu alimpenda Daudi. Na Daudi akamwomba Mungu amruhusu ajenge Hekalu kwa ajili ya watu wa Israeli Lakini Sulemani ndiye aliyemjengea Mungu Hekalu. Lakini Mungu Aliye Juu sana hahitaji yumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu ili aishi ndani yake. Nabii aliandika hivi: ‘Bwana asema, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni sehemu ya kuweka miguu yangu. Hivyo mnadhani mnaweza kunijengea nyumba? Je, ninahitaji mahali pa kupumzika? Kumbukeni, niliumba vitu vyote hivi?’” Kisha Stefano akasema, “Enyi viongozi wa Kiyahudi mlio wakaidi! Mnakataa kumpa Mungu mioyo yenu na mnakataa hata kumsikiliza. Daima mko kinyume na Roho Mtakatifu. Baba zenu walikuwa vivyo hivyo, nanyi mko kama wao! Walimtesa kila nabii aliyewahi kuishi. Waliwaua hata wale ambao zamani zilizopita walisema kwamba Mwenye Haki ilikuwa aje. Na sasa mmekuwa kinyume na Mwenye Haki na mmemwua. Ninyi ndiyo mliipokea Sheria ya Mungu, aliyoitoa kupitia malaika zake. Lakini hamtaki kuitii!” Waliokuwa kwenye mkutano wa baraza waliposikia maneno haya, walikasirika sana na wakamsagia meno Stefano kwa hasira. Lakini Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alitazama juu mbinguni, na kuuona utukufu wa Mungu. Alimwona Yesu amesimama upande wa kulia wa Mungu. Stefano akasema, “Tazama! Naona mbingu zimefunguka. Na ninamwona Mwana wa Adamu amesimama upande wa kulia wa Mungu.” Kila mmoja pale akaanza kupiga kelele, wakaziba masikio yao kwa mikono yao. Wote kwa pamoja wakamvamia Stefano. Wakamtoa nje ya mji na kuanza kumpiga kwa mawe. Mashahidi walioshuhudia uongo kinyume cha Stefano waliacha makoti yao kwa kijana aliyeitwa Sauli. Walipokuwa wanampiga kwa mawe, Stefano aliomba, akisema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” Alianguka kwa magoti yake na kupaza sauti, akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii!” Haya yalikuwa maneno yake ya mwisho kabla ya kufa. Sauli aliridhia kuwa kuuawa kwa Stefano lilikuwa jambo jema. Baadhi ya wacha Mungu walimzika Stefano, wakaomboleza na kumlilia kwa sauti kuu. Kuanzia siku hiyo Wayahudi walianza kulitesa sana kanisa na waamini katika mji wa Yerusalemu. Sauli pia alijaribu kuliharibu kanisa. Aliingia katika nyumba za waamini, akawaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Waamini wote walikimbia kutoka Yerusalemu, mitume peke yao ndiyo walibaki. Waamini walikwenda mahali tofauti tofauti katika Uyahudi na Samaria. *** *** Walitawanyika kila mahali, na kila walikokwenda waliwahubiri watu Habari Njema. Filipo alikwenda katika mji mkuu wa jimbo la Samaria na kuwahubiri watu kuhusu Masihi. Watu wa Samaria walimsikiliza Filipo na kuona miujiza aliyotenda. Wote walisikiliza kwa makini yale aliyosema. Watu wengi miongoni mwao walikuwa na mapepo, lakini Filipo aliyakemea mapepo na yaliwatoka watu. Mapepo yalipiga kelele nyingi yalipokuwa yanawatoka watu. Walikuwepo pia watu wengi waliopooza na walemavu wa miguu pale. Filipo aliwaombea na wote walipona. Kulikuwa furaha kubwa katika mji ule wa Samaria siku ile! Mtu mmoja aliyeitwa Simoni alikuwa anaishi katika mji huo. Kabla Filipo hajaenda huko, Simoni alikuwa akifanya uchawi na kuwashangaza watu wote wa Samaria. Alijigamba na kujiita mtu mkuu. Watu wote, kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliamini yale aliyosema Simoni. Walisema, “Mtu huyu ndiye anayeitwa ‘Nguvu Kuu ya Mungu.’” Simoni aliwashangaza watu kwa muda mrefu kwa uchawi wake na watu wote wakawa wafuasi wake. Lakini Filipo alipowahubiri watu Habari Njema kuhusu Ufalme wa Mungu na Nguvu za Yesu Kristo. Wanaume na wanawake waliamini alichosema Filipo na wakabatizwa. Simoni mwenyewe aliamini, na baada ya kubatizwa, alikaa karibu na Filipo. Alipoona miujiza na matendo makuu ya ajabu yaliyofanyika kupitia Filipo, alishangaa. Mitume mjini Yerusalemu, waliposikia kuwa watu wa Samaria wameupokea Ujumbe wa Mungu, waliwatuma Petro na Yohana kwenda kwa watu wa Samaria. Petro na Yohana walipofika, waliomba ili Roho Mtakatifu awashukie waamini wa Samaria. Watu hawa walikuwa wamebatizwa katika jina la Bwana Yesu, lakini Roho Mtakatifu alikuwa bado hajamshukia hata mmoja wao. Na hii ndiyo sababu Petro na Yohana waliomba. Mitume hawa wawili walipoweka mikono yao juu ya watu, Roho Mtakatifu aliwashukia. Simoni aliyekuwa mchawi alipoona Roho Mtakatifu anatolewa kwa watu kwa kuweka mikono juu yao. Aliwapa pesa mitume. Akasema, “Nipeni na mimi nguvu hii ili nitakapoweka mikono yangu juu ya mtu yeyote, atampata Roho Mtakatifu.” Petro akamwambia Simoni, “Wewe pamoja na pesa zako mwangamie kwa sababu unadhani unaweza kununua karama kutoka kwa Mungu kwa pesa. Huwezi kushirikiana nasi katika kazi hii. Moyo wako si safi mbele za Mungu. Badili moyo wako! Achana na mawazo haya maovu na umwombe Bwana. Yumkini atakusamehe! Kwa kuwa ninaona umejaa wivu mwingi nawe ni mfungwa wa uovu.” Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili haya uliyosema yasinipate.” Ndipo wale mitume wawili waliwaambia watu waliyoona Yesu akitenda. Wakawaambia ujumbe wa Bwana. Kisha wakarudi Yerusalemu. Wakiwa njiani kurudi, walipitia katika miji mingi ya Wasamaria na kuwahubiri watu Habari Njema. Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jiandae na uende kusini katika barabara ya jangwani inayoteremka kutoka Yerusalemu kwenda Gaza.” Filipo alijiandaa na kwenda. Akiwa njiani alimwona mwanaume kutoka Ethiopia. Alikuwa towashi na ofisa muhimu wa Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa na mweka hazina mkuu wa malkia. Mtu huyu alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu. Na alikuwa anarudi Ethiopia. Alikuwa ameketi katika gari lake la kukokotwa na farasi akiwa anasoma kitabu cha nabii Isaya. Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye gari hilo na uwe karibu yake.” Hivyo Filipo akaenda karibu na gari, akamsikia mtu yule akisoma kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamwuliza, “Unaelewa unachosoma?” Yule mtu akajibu, “Nitaelewaje? Ninahitaji mtu wa kunifafanulia.” Ndipo akamwomba Filipo apande garini na aketi pamoja naye. Sehemu ya Maandiko aliyokuwa anasoma ilikuwa hii: “Alikuwa kama kondoo anayepelekwa kwa mchinjaji. Alikuwa kama mwana kondoo asivyopiga kelele anapokatwa manyoya yake. Hakusema kitu. Alidhalilishwa, na kunyimwa haki zake zote. Maisha yake duniani yamekoma. Hivyo hakutakuwa simulizi yoyote kuhusu wazaliwa wake.” Afisa akamwambia Filipo, “Tafadhali niambie, nabii anazungumza kuhusu nani? Anazungumza kuhusu yeye mwenyewe au mtu mwingine?” Filipo akaanza kuzungumza. Alianzia na Andiko hili na kumwambia mtu yule Habari Njema kuhusu Yesu. Walipokuwa wanasafiri waliyakuta maji mahali fulani. Afisa akasema, “Tazama! Hapa kuna maji! Nini kinanizuia nisibatizwe?” *** Ndipo Afisa akaamuru gari lake lisimame. Wote wawili, Filipo na Afisa, wakatelemka wakaingia kwenye maji na Filipo akambatiza towashi. Walipotoka kwenye maji, Roho wa Bwana akamchukua Filipo; afisa hakumwona Filipo tena. Afisa aliendelea na safari yake kurudi nyumbani, akiwa mwenye furaha sana. Lakini Filipo alionekana katika mji ulioitwa Azoto. Alikuwa akienda kwenye mji wa Kaisaria. Aliwahubiri watu Habari Njema katika miji yote wakati anasafiri kutoka Azoto kwenda Kaisaria. Huko Yerusalemu Sauli aliendelea kuwatisha wafuasi wa Bwana, na hata kuwaambia kuwa angewaua. Alikwenda kwa kuhani mkuu, na kumwomba aandike barua kwenda kwenye masinagogi yaliyokuwa katika mji wa Dameski. Sauli alitaka kuhani mkuu ampe mamlaka ya kuwatafuta watu katika mji wa Dameski waliokuwa wafuasi wa Njia ya Bwana. Ikiwa angewapata waamini huko, wanaume au wanawake, angewakamata na kuwaleta Yerusalemu. Hivyo Sauli alikwenda Dameski. Alipoukaribia mji, ghafla mwanga mkali kutoka mbinguni ukaangaza kumzunguka. Akadondoka chini na akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli! Kwa nini unanitesa?” Sauli akasema, “Wewe ni nani, Bwana?” Sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu, unayemtesa. Simama sasa na uingie mjini. Mtu mmoja huko atakueleza unachopaswa kufanya.” Wanaume waliokuwa wanasafiri pamoja na Sauli walisimama pale kimya. Waliisikia sauti, lakini hawakumwona yeyote. Sauli alisimama kutoka chini na kufumbua macho yake, lakini hakuweza kuona. Hivyo wale aliokuwa nao wakamshika mkono na kumwongoza kuingia Dameski. Kwa siku tatu Sauli hakuweza kuona; hakula wala kunywa. Alikuwepo mfuasi wa Yesu katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania. Katika maono Bwana alimwita, “Anania!” Anania alijibu, “Niko hapa, Bwana.” Bwana akamwambia, “Amka na uende katika mtaa unaoitwa Mtaa Ulionyooka. Tafuta nyumba ya Yuda na uliza kuhusu mtu anayeitwa Sauli anayetoka katika mji wa Tarso. Yuko katika nyumba hiyo sasa, anaomba. Ameoneshwa katika maono kuwa mtu anayeitwa Anania anamwendea na kuweka mikono juu yake ili aweze kuona tena.” Lakini Anania akajibu, “Bwana, watu wengi wameniambia kuhusu mtu huyu. Wameniambia kuhusu mambo mengi mabaya aliyowatendea watu wako watakatifu katika mji wa Yerusalemu. Na sasa amekuja hapa Dameski. Viongozi wa makuhani wamempa mamlaka ya kuwakamata watu wote wanaokuamini wewe.” Lakini Bwana Yesu akamwambia Anania, “Nenda, nimemchagua Sauli kwa kazi maalumu. Ninataka ayahubiri mataifa mengine, watawala na watu wa Israeli kuhusu mimi. Nitamwonyesha yote ambayo lazima atateseka kwa ajili yangu.” Hivyo Anania aliondoka na kwenda nyumbani kwa Yuda. Akaweka mikono yake juu ya Sauli na kusema, “Sauli, ndugu yangu, Bwana Yesu amenituma. Ndiye uliyemwona barabarani wakati ukija hapa. Amenituma ili uweze kuona tena, pia ujazwe Roho Mtakatifu.” Ghafla, vitu kama magamba ya samaki vikaanguka kutoka kwenye macho ya Sauli. Akaanza kuona tena! Kisha akasimama na kwenda kubatizwa. Baada ya kula chakula, akaanza kujisikia kuwa na nguvu tena. Sauli alikaa pamoja na wafuasi wa Yesu katika mji wa Dameski kwa siku chache. Baadaye alianza kwenda katika masinagogi na kuwahubiri watu kuhusu Yesu. Aliwaambia watu, “Yesu ni Mwana wa Mungu!” Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa. Wakaulizana, “Je, huyu si yule aliyekuwa anajaribu kuwaangamiza watu wanaomwamini Yesu katika mji wa Yerusalemu? Na hakuja hapa ili awakamate wafuasi wa Yesu na kuwarudisha kwa viongozi wa makuhani?” Lakini Sauli aliendelea kuwa nguvu katika kuthibitisha kwamba Yesu ndiye Masihi. Uthibitisho wake ulikuwa na nguvu kiasi kwamba Wayahudi walioishi Dameski hawakuweza kubishana naye. Baada ya siku nyingi kupita, baadhi ya Wayahudi waliweka mpango wa kumwua Sauli. Waliyalinda malango ya mji usiku na mchana. Walitaka kumwua Sauli, lakini aliambiwa kuhusu mpango wao. Usiku mmoja baadhi ya wafuasi ambao Sauli aliwafundisha walimsaidia kuondoka mjini. Walimweka katika kikapu, wakamtoa kwa kumshusha kupitia kwenye tundu lililokuwa kwenye ukuta wa mji. Kisha Sauli alikwenda Yerusalemu. Akajaribu kujiunga na kundi la wafuasi, lakini wote walimwogopa. Hawakuamini kuwa naye amekuwa mfuasi wa Yesu. Lakini Barnaba alimkubali Sauli, akamchukua na kumpeleka kwa mitume. Akawaeleza namna ambavyo Sauli alimwona Bwana akiwa njiani na namna ambavyo Bwana aliongea naye. Kisha akawaambia namna ambavyo Sauli amehubiri kwa ujasiri kuhusu Yesu katika mji wa Dameski. Sauli alikaa na wafuasi na kwenda kila mahali katika mji wa Yerusalemu akihubiri kwa ujasiri kwa ajili ya Bwana. Kila mara alibishana na Wayahudi waliokuwa waliozungumza Kiyunani, ambao walianza kutengeneza mpango wa kumwua. Waamini walipoujua mpango huu, walimchukua Sauli mpaka Kaisaria, na kutoka huko walimsafirisha mpaka katika mji wa Tarso. Kanisa katika Uyahudi yote, Galilaya na Samaria likawa na wakati wa amani. Na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, vikundi hivi vya waamini vikawa na nguvu katika imani na kuonesha utii kwa ajili ya Bwana kwa namna walivyoishi. Hivyo kanisa kila mahali liliongezeka kwa idadi. Petro alikuwa akisafiri katika sehemu zote za Uyahudi, Galilaya na Samaria, na akasimama kuwatembelea waamini walioishi Lida. Huko alikutana na mtu aliyeitwa Ainea, ambaye alikuwa amepooza na hakuweza kutoka kitandani kwa miaka nane. Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo amekuponya. Simama na kiweke kitanda chako vizuri!” Ainea alisimama saa ile ile. Watu wote walioishi Lida na tambarare ya Sharoni walimwona, na wakaamua kumfuata Bwana. Katika mji wa Yafa kulikuwa na mfuasi wa Yesu aliyeitwa Tabitha, Jina lake kwa Kiyunani lilikuwa Dorkasi. Daima aliwatendea watu mambo mema na kuwapa pesa wale wenye mahitaji. Petro alipokuwa Lida, Tabitha aliugua na kufa. Waliusafisha mwili wake na kuuweka chumbani ghorofani. Wafuasi waliokuwa Yafa wakasikia kuwa Petro yuko Lida, mji ambao haukuwa mbali na Yafa. Hivyo waliwatuma watu wawili, waliomsihi Petro wakisema, “Tafadhali njoo kwetu haraka!” Petro alijiandaa na kwenda pamoja nao. Alipofika, walimchukua na kumpeleka kwenye chumba ghorofani. Wajane wote walisimama wakamzunguka huku wakilia na wakamwonesha mavazi ambayo Tabitha alitengeneza alipokuwa hai. Petro akawatoa watu wote chumbani. Akapiga magoti na kuomba. Kisha akaugeukia mwili wa Tabitha na kusema, “Tabitha! Simama.” Akafumbua macho yake. Alipomwona Petro akaketi. Petro akamshika mkono na akamsaidia kusimama. Ndipo akawaita waamini na wajane chumbani. Akawaonyesha Tabitha; akiwa hai! Watu kila mahali katika mji wa Yafa wakatambua kuhusu hili, na wengi wakamwamini Bwana. Petro alikaa Yafa siku nyingi nyumbani kwa mtu mmoja aitwaye Simoni, aliyekuwa mtengenezaji wa ngozi. Kulikuwa mtu aliyeitwa Kornelio katika mji wa Kaisaria. Mtu huyu alikuwa ofisa wa kikosi kilichoitwa “Kikosi cha Kiitalia” katika jeshi la Rumi. Alikuwa mcha Mungu. Yeye na watu wengine wote walioishi katika nyumba yake walikuwa wanamwabudu Mungu wa kweli. Alitoa pesa zake nyingi kuwasaidia maskini miongoni mwa Wayahudi na daima alimwomba Mungu kwa kufuata utaratibu kama ilivyokuwa. Mchana mmoja yapata saa tisa, kwa uwazi na dhahiri Kornelio aliona maono. Alimwona malaika kutoka kwa Mungu akimwendea na akamwambia, “Kornelio!” Akiwa anashangaa na kuogopa, Kornelio akasema, “Unataka nini, bwana?” Malaika akamwambia, “Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako unazowapa maskini. Anakukumbuka kwa yote uliyotenda. Tuma baadhi ya watu sasa waende katika mji wa Yafa wakamlete mtu anayeitwa Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. Anakaa kwa mtu ambaye naye pia anaitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko kwenye ufukwe wa bahari.” Malaika aliyeongea na Kornelio akaondoka. Ndipo Kornelio aliita watumishi wake wawili na askari mmoja. Askari alikuwa mcha Mungu, mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. Kornelio akawaelekeza kila kitu watu hawa watatu kisha akawatuma kwenda Yafa. Siku iliyofuata wakati wa adhuhuri walipokuwa wanaukaribia mji wa Yafa, Petro alipanda juu ya paa kuomba. Alihisi njaa na akataka chakula. Lakini walipokuwa wanamwandalia chakula ili ale, aliona maono. Aliona mbingu zikifunguka na kitu kama shuka kubwa kikishushwa chini kutoka mbinguni kwa pembe nne. Ndani yake mlikuwa aina zote za wanyama, watambaao na ndege. Kisha sauti ikamwambia, “Petro simama uchinje chochote hapa kisha ule.” Lakini Petro akasema, “Siwezi kufanya hivyo, Bwana! Sijawahi kula kitu chochote kisicho safi au kisicho stahili kutumiwa kwa chakula.” Lakini sauti ikamwambia tena, “Mungu amekwisha vitakasa vitu vyote hivi. Usiseme havistahili kuliwa.” Hili lilimtokea mara tatu. Kisha likachukuliwa mbinguni. Petro alijiuliza maono haya yalikuwa na maana gani. Watu ambao Kornelio aliwatuma walishaiona nyumba ya Simoni na walikuwa wamesimama mlangoni. Waliuliza, “Je, Simoni Petro yuko hapa?” Petro akiwa bado anafikiri kuhusu maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Sikiliza, kuna watu watatu wanakutafuta. Inuka na ushuke chini. Nenda nao, usisite, kwa sababu nimewatuma.” Hivyo Petro akashuka chini na kuwaambia, “Nafikiri mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja hapa?” Wale watu wakasema, “Malaika mtakatifu amemwambia Kornelio akualike nyumbani mwake. Ni mtu mwema na hutenda kwa haki, na anamwabudu Mungu na Wayahudi wote wanamheshimu. Malaika alimwambia akualike nyumbani kwake ili asikilize yale utakayosema.” Petro akawakaribisha ndani watu wale ili walale usiku huo. Siku iliyofuata Petro alijiandaa na kuondoka na wale watu watatu. Baadhi ya waamini katika mji wa Yafa walikwenda pamoja naye. Siku iliyofuata walifika katika mji wa Kaisaria. Kornelio alikuwa anawasubiri na alikuwa amewakusanya jamaa na rafiki zake wa karibu nyumbani mwake. Petro alipoingia ndani ya nyumba, Kornelio alimlaki kisha akaanguka miguuni kwa Petro na akamwabudu. Lakini Petro akamwambia asimame. Petro akasema, “Simama! Mimi ni mtu tu kama wewe.” Petro aliendelea kuzungumza na Kornelio. Ndipo Petro akaingia ndani na kuona kundi kubwa la watu wamekusanyika pale. Petro akawaambia watu wale kuwa, “Mnaelewa kuwa ni kinyume na sheria yetu kwa Myahudi kushirikiana au kumtembelea mtu ambaye si Myahudi. Lakini Mungu amenionyesha kuwa nisimchukulie mtu yeyote kuwa yu kinyume na desturi za Kiyahudi. Ndiyo sababu sikubisha watu wenu waliponiambia kuja hapa. Sasa, tafadhali niambieni kwa nini mmeniita hapa.” Kornelio akasema, “Siku nne zilizopita, kama saa tisa mchana nilikuwa ninaomba ndani ya nyumba yangu. Ghafla akawepo mtu mmoja amesimama mbele yangu amevaa mavazi meupe yanayong'aa. Akasema, ‘Kornelio, Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako kwa maskini. Anakukumbuka wewe na yote uliyofanya. Hivyo tuma baadhi ya watu kwenye mji wa Yafa na wamwambie Simoni Petro kuja. Anakaa na mtu mwingine anayeitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko pembeni mwa bahari.’ Hivyo nikawatuma kwako haraka. Imekuwa vizuri sana umekuja hapa. Sasa sote tupo hapa mbele za Mungu na tuko tayari kusikia kila kitu ambacho Bwana amekwamuru utuambie.” Petro akaanza kwa kusema: “Hakika sasa ninaelewa ni kwa nini Mungu hawachukulii kundi fulani la watu kuwa bora kuliko wengine. Anamkubali yeyote anayemwabudu na anayetenda haki. Haijalishi wanatoka katika taifa lipi. Mungu amezungumza na watu wa Israeli. Aliwaletea Habari Njema kwamba amani imekuja kupitia Yesu Kristo ambaye ndiye Bwana wa watu wote. Mnafahanu kilichotokea katika Uyahudi yote. Kilianzia Galilaya baada ya Yohana kuwaambia watu kuwa inawapasa kubatizwa. Mnajua kuhusu Yesu kutoka Nazareti. Mungu alimfanya Masihi kwa kumpa Roho Mtakatifu na nguvu. Yesu alikwenda kila mahali akiwatendea mema watu. Akawaponya wale waliokuwa wakitawaliwa na yule Mwovu, akionyesha kuwa Mungu alikuwa pamoja naye. Tuliona yote ambayo Yesu alitenda katika Uyahudi na katika mji wa Yerusalemu. Lakini aliuawa. Walimpigilia kwenye msalaba uliotengenezwa kwa mti. Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, Mungu alimfufua na kumfanya aonekane wazi wazi. Hakuonekana kwa Wayahudi wote, lakini alionekana kwetu sisi tu, ambao Mungu tayari alikwisha kutuchagua tuwe mashahidi. Tulikula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu. Yesu alitwambia twende na kuwaeleza watu. Alituagiza tuwaeleza kwamba yeye ndiye ambaye Mungu amemchagua kuwa mwamuzi wa wote walio hai na wote walio kufa. Na ya kwamba kila atakayemwamini Yesu, atasamehewa dhambi zake kupitia nguvu jina Lake. Manabii wote wanakubali kuwa jambo hili ni la kweli.” Petro alipokuwa bado anazungumza, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanamsikiliza. Waamini wa Kiyahudi waliofuatana na Petro walishangaa kwamba Roho Mtakatifu amemiminwa kama zawadi hata kwa watu wasio Wayahudi. Waliwasikia wakiongea lugha mbalimbali na kumsifu Mungu. Ndipo Petro akasema, “Je, mtu yeyote anawezaje kuzuia watu hawa wasibatizwe katika maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea!” Hivyo Petro akawaambia wambatize Kornelio pamoja na jamaa zake na rafiki zake katika jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba Petro akae nao kwa siku chache. Mitume na waamini katika Uyahudi walisikia kwamba watu wasio Wayahudi wameyapokea mafundisho ya Mungu pia. Lakini Petro alipokuja Yerusalemu, baadhi ya waamini wa Kiyahudi walimkosoa. Walisema, “Uliingia katika nyumba za watu wasio Wayahudi ambao hawajatahiriwa na ukala pamoja nao!” Hivyo Petro akawaelezea namna ilivyotokea. Akasema, “Nilikuwa katika mji wa Yafa. Nilipokuwa nikiomba, niliona maono. Niliona kitu kikishuka chini kutoka mbinguni. Kilionekana kama shuka kubwa ikishushwa chini kwa pembe zake nne. Kikaja chini karibu yangu. Nilipotazama ndani yake, niliona aina zote za wanyama, pamoja na wale wa porini, wanyama wanaotambaa na ndege. Nilisikia sauti ikiniambia. Chinja chochote hapa na ule!” “Lakini nilisema, ‘Siwezi kufanya hivyo Bwana! Sijawahi kula kitu cho chote kisicho safi au kisichostahili kuliwa kama chakula.’ Lakini sauti kutoka mbinguni ikajibu tena, ‘Mungu amevitakasa vitu hivi. Usiseme havistahili kuliwa!’ Hili lilitokea mara tatu. Ndipo kitu chote kikachukuliwa kurudi mbinguni. Saa hiyo hiyo baada ya hayo wakawepo watu watatu wamesimama nje ya nyumba nilimokuwa ninakaa. Walikuwa wametumwa kutoka Kaisaria kunichukua. Roho Mtakatifu aliniambia niende nao bila kuwa na mashaka. Ndugu hawa hapa sita walikwenda pamoja nami, na tulikwenda katika nyumba ya Kornelio. Alitwambia kuhusu malaika aliyemwona amesimama katika nyumba yake. Malaika alimwambia, ‘Tuma baadhi ya watu waenda Yafa kumchukua Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. Atazungumza na wewe. Ujumbe atakaokwambia utakuokoa wewe na kila mtu anayeishi katika nyumba yako.’ Nilipoanza kuzungumza, Roho Mtakatifu alikuja juu yao kama vile alivyokuja juu yetu mwanzo. Ndipo nilikumbuka maneno ya Bwana Yesu, aliyosema: ‘Yohana alibatiza katika maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ Mungu amewapa watu hawa karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo. Hivyo ningewezaje kupinga yale ambayo Mungu alitaka kufanya?” Waamini wa Kiyahudi waliposikia hili, wakaacha kubisha. Wakamsifu Mungu na kusema, “Kwa hiyo Mungu anawaruhusu watu wasio Wayahudi kubadili mioyo yao na kuwa na maisha anayotoa!” Waamini walitawanyika kwa sababu ya mateso yaliyoanza baada ya Stefano kuuawa. Baadhi ya waamini walikwenda mbali mpaka Foeniki, Kipro na Antiokia. Walihubiri Habari Njema katika maeneo haya, lakini kwa Wayahudi tu. Baadhi ya waamini hawa walikuwa watu kutoka Kipro na Kirene. Watu hawa walipofika Antiokia, walianza kuwahubiri watu wasio Wayahudi. Waliwahubiri Habari Njema kuhusu Bwana Yesu. Nguvu ya Bwana iliambatana na watu hawa, na idadi kubwa ya watu waliamini na kuamua kumfuata Bwana. Kanisa katika mji wa Yerusalemu liliposikia kuhusu hili, lilimtuma Barnaba kwenda Antiokia. Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu na imani. Alipokwenda Antiokia na kuona jinsi Mungu alivyowabariki waamini pale, alifurahi sana. Akawatia moyo wote, akasema, “Iweni waaminifu kwa Bwana daima. Mtumikieni Yeye kwa mioyo yenu yote.” Watu wengi zaidi wakawa wafuasi wa Bwana. *** Kisha Barnaba alikwenda katika mji wa Tarso kumtafuta Sauli. Alipompata, alimpeleka Antiokia. Walikaa pale mwaka mzima. Kila wakati kanisa lilipokusanyika, Barnaba na Sauli walikutana nao na kuwafundisha watu wengi. Ni katika mji wa Antiokia ambako wafuasi wa Bwana Yesu walianza kuitwa “Wafuasi wa Kristo”. Katika wakati huo huo baadhi ya manabii walitoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. Mmoja wao, aliyeitwa Agabo, huku akisaidiwa na Roho Mtakatifu, alisimama na kuzungumza. Alisema, “Wakati mbaya sana unakuja katika dunia yote. Hakutakuwa chakula kwa ajili ya watu kula.” (Kipindi hiki cha njaa kilitokea Klaudio alipokuwa mtawala wa Kirumi) Wafuasi wa Bwana wakaamua kwamba kila mmoja wao atatuma kiasi anachoweza kuwasaidia ndugu wote wanaoishi Uyahudi. Walikusanya pesa na kuwapa Barnaba na Sauli, waliozipeleka kwa wazee, katika Uyahudi. Katika wakati huu huu, Mfalme Herode akaanza kuwatesa baadhi ya waamini waliokuwa sehemu ya kanisa. Aliamuru Yakobo aliyekuwa kaka yake Yohana, auawe kwa upanga. Herode alipoona kuwa Wayahudi wamelifurahia jambo hili, aliamua kumkamata Petro pia. Hii lilitokea katika kipindi cha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Alimkamata Petro na kumfunga gerezani, ambako alilindwa na kundi la askari kumi na sita. Herode alipanga kumleta Petro mbele ya watu ili ahukumiwe, lakini alisubiri mpaka baada ya sikukuu ya Pasaka. Hivyo Petro aliwekwa gerezani lakini kanisa lilikuwa likiomba kwa Mungu bila kuacha kwa ajili yake. Wakati wa usiku kabla ya siku ambayo Herode alipanga kumhukumu mbele ya watu, Petro, akiwa amefungwa minyororo miwili, alikuwa amelala katikati ya askari wawili. Na askari waliokuwa nje ya mlango walikuwa wanalinda gereza. Ghafla malaika wa Bwana alikuwa amesimama pale, na chumba kilijaa mwanga. Malaika akamwamsha Petro kwa kumpiga upande, akasema, “Amka haraka!” Minyororo ikaanguka kutoka mikono mwa Petro. Malaika akasema, “Vaa nguo na viatu vyako.” Petro alifanya kama alivyoambiwa. Kisha malaika akasema, “Vaa koti lako na unifuate.” Hivyo malaika akatoka nje na Petro alimfuata. Hakujua kama kweli malaika alikuwa anafanya hili. Alidhani alikuwa anaona maono. Petro na malaika wakavuka lindo la kwanza na lindo la pili. Kisha walifika kwenye lango la chuma lililowatenganisha na mji. Lango likafunguka. Baada ya kuvuka lango na kutembea umbali wa kama mtaa mmoja, malaika akatoweka ghafla. Ndipo Petro akatambua kuwa haikuwa ndoto. Akawaza moyoni akisema, “Sasa ninajua kwamba Bwana hakika alimtuma malaika wake kwangu. Ameniokoa kutoka kwa Herode na kutoka kwenye mabaya yote ambayo Wayahudi walidhani yatanipata.” Petro alipotambua hili, alikwenda nyumbani kwa Mariamu, mama yake Yohana, aliyeitwa Marko. Watu wengi walikuwa wamekusanyika pale wakiomba. Petro alibisha kwenye mlango wa nje. Mtumishi wa kike aliyeitwa Rhoda alikuja ili afungue mlango. Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi sana hata akasahau kufungua mlango. Akakimbilia ndani na kuliambia kundi, “Petro yuko mlangoni!” Waamini wakamwambia, “Wewe una kichaa!” Lakini alipoendelea kusema kwamba ni kweli Petro yuko mlangoni. Waamini walisema, “Lazima atakuwa malaika wa Petro.” Lakini Petro aliendelea kubisha mlangoni. Waamini walipoufungua mlango na kumwona, wakashangaa. Petro akawafanyia ishara kwa mkono wake kuwaambia wanyamaze. Akawaeleza namna Bwana alivyomtoa nje ya gereza. Akasema, “Mwambieni Yakobo na ndugu wengine kilichotokea.” Kisha akawaacha na kwenda sehemu nyingine. Siku iliyofuata askari walichanganyikiwa. Walijiuliza nini kimempata Petro. Herode alimtafuta kila mahali lakini hakumpata. Hivyo aliwahoji walinzi na kuamuru wauawe. Baadaye, Herode alihama kutoka Uyahudi na kwenda katika mji wa Kaisaria na kukaa huko kwa muda. Herode aliwakasirikia sana watu katika miji ya Tiro na Sidoni. Lakini miji hii ilihitaji chakula kutoka katika nchi yake, hivyo baadhi yao walimjia wakitaka amani naye. Waliweza kumshawishi Blasto mtumishi binafsi wa Mfalme ili awasaidie. Herode alichagua siku maalumu ya kukutana nao. Siku hiyo alivaa vazi zuri la kifalme. Aliketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu. Watu wakapaza sauti zao na kusema, “Hii ni sauti ya mungu, siyo mwanadamu!” Herode hakumpa Mungu utukufu. Hivyo malaika wa bwana akampiga kwa ugonjwa. Akaliwa na minyoo ndani na kufa. Ujumbe wa Mungu ulikuwa unasambaa, ukiwafikia watu wengi zaidi. Baada ya Barnaba na Sauli kumaliza kazi yao Yerusalemu, walirudi Antiokia, walimchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Walikuwepo baadhi ya manabii na walimu katika kanisa la Antiokia. Walikuwa Barnaba, Simeoni (ambaye pia aliitwa Nigeri ), Lukio (kutoka mji wa Kirene), Manaeni (aliyekua pamoja na Mfalme Herode ), na Sauli. Watu hawa wote kwa pamoja walikuwa wanamwabudu Bwana na wamefunga Roho Mtakatifu alipowaambia, “Nitengeeni Barnaba na Sauli ili wanifanyie kazi maalumu. Wao ndio niliowachagua kuifanya kazi hiyo.” Hivyo kanisa lilifunga na kuomba. Wakaweka mikono yao juu ya Barnaba na Sauli, wakaagana nao na kuwaacha waende. Barnaba na Sauli walitumwa na Roho Mtakatifu. Walikwenda katika mji wa Seleukia. Kutoka hapo walitweka tanga na kusafiri mpaka kwenye kisiwa cha Kipro. Barnaba na Sauli walipofika kwenye mji wa Salami, walihubiri ujumbe wa Mungu katika masinagogi ya Kiyahudi. Yohana ambaye pia anaitwa Marko alikuwa pamoja nao ili kuwasaidia. Walisafiri wakitisha kisiwa chote mpaka kwenye mji wa Pafo. Huko walimkuta mwanaume wa Kiyahudi aliyeitwa Bar-Yesu aliyekuwa akifanya uchawi. Alikuwa nabii wa uongo. Alikaa daima karibu na Sergio Paulo, aliyekuwa gavana na mtu makini sana. Sergio Paulo aliwaalika Barnaba na Sauli waende kumtembelea kwa sababu alitaka kusikia ujumbe wa Mungu. Lakini mchawi Elima (Bar-Yesu kama alivyoitwa kwa Kiyunani) alizungumza kinyume nao ili kuwapinga, akijaribu kumzuia gavana asimwamini Yesu. Kisha Sauli (ambaye pia anajulikana kama Paulo), akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkazia macho Elima na kusema, “Ewe mwana wa Ibilisi, uliyejaa uongo na aina zote za hila za uovu! Wewe ni adui wa kila kilicho cha kweli. Hautaacha kuzibadili kweli za Bwana kuwa uongo? Sasa Bwana atakugusa na utakuwa asiyeona. Hautaweza kuona kitu chochote kwa muda, hata mwanga wa jua.” Ndipo kila kitu kikawa giza kwa Elima. Akazunguka kila mahali na akapotea. Alikwenda kila mahali akijaribu kumpata mtu wa kumshika mkono ili amwongoze. Gavana alipoyaona haya, akaamini. Akayashangaa mafundisho kuhusu Bwana. Paulo na watu waliokuwa pamoja naye walitweka tanga na kusafiri kwa merikebu kutoka Pafo mpaka Perge, mji uliokuwa Pamfilia. Hapo Yohana Marko aliwaacha na akarudi Yerusalemu. Waliendelea na safari yao kutoka Perge na kwenda Antiokia, mji karibu na Pisidia. Siku ya Sabato walikwenda katika sinagogi la Kiyahudi na kuketi chini. Sheria ya Musa na maandishi ya manabii vilisomwa. Kisha viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe Paulo na Barnaba, wakisema, “Ndugu zetu, ikiwa mna kitu chochote cha kusema kitakachowasaidia watu hapa, tafadhali semeni.” Paulo akasimama, akanyoosha mkono wake ili wamsikilize, akasema, “Watu wa Israeli nanyi nyote msio Wayahudi mnaomwabudu Mungu wa kweli, tafadhali nisikilizeni! Mungu wa Israeli aliwachagua baba zetu. Na watu wetu walipoishi Misri kama wageni, aliwafanya wakuu. Kisha akawatoa katika nchi ile kwa nguvu kuu. Aliwavumilia kwa miaka arobaini walipokuwa jangwani. Mungu aliangamiza mataifa saba katika nchi ya Kanaani na kuwapa nchi yao watu wake. Yote haya yalitokea katika kipindi cha kadiri ya miaka mia nne na hamsini. Baada ya hili, Mungu akawapa watu wetu waamuzi kuwaongoza mpaka wakati wa nabii Samweli. Ndipo watu wakaomba kuwa na mfalme. Mungu akawapa Sauli, mwana wa Kishi. Sauli alitoka katika kabila la Benjamini. Alikuwa mfalme kwa miaka arobaini. Baada ya Mungu kumwondoa Sauli katika ufalme, Mungu alimfanya Daudi kuwa Mfalme wao. Hiki ndicho Mungu alisema kuhusu Daudi: ‘Daudi, mwana wa Yese, ni mtu ambaye Mimi mwenyewe nimemchagua. Atafanya kila kitu nitakachotaka afanye.’ Kama alivyoahidi, Mungu amemleta mmoja wa wazao wa Daudi katika Israeli ili awe Mwokozi wao, mzao huyo wa Daudi ni Yesu. Kabla Yesu hajaja, Yohana aliwaambia watu wote wa Israeli wanachopaswa kufanya. Waliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa walitaka kubadili maisha yao. Yohana alipokuwa anamaliza kazi yake, alisema, ‘Mnadhani mimi ni nani? Mimi siyo Masihi. Masihi atakuja baadaye, nami sistahili kuwa mtumwa wake wa kufungua kamba za viatu vyake.’ Ndugu zangu, wana katika familia ya Ibrahimu na ninyi watu wengine ambao pia mnamwabudu Mungu wa kweli, sikilizeni! Habari kuhusu wokovu huu imeletwa kwetu. Wayahudi waishio Yerusalemu na viongozi wao hawakutambua kuwa Yesu ni Mwokozi. Maneno ambayo manabii waliandika kuhusu yeye yalikuwa yakisomwa kila siku ya Sabato, lakini hawakuyaelewa. Walimhukumu Yesu. Walipofanya hivi, waliyatimiliza maneno ya manabii. Hawakupata sababu ya msingi kwa nini Yesu afe, lakini walimwomba Pilato amwue. Wayahudi hawa walimtendea Yesu mambo yote mabaya ambayo Maandiko yalisema yangempata Yesu. Kisha walimteremsha Yesu kutoka msalabani na kumweka kaburini. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu! Baada ya hili, kwa siku nyingi, wale waliofuatana na Yesu kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu walimwona. Wao sasa ni mashahidi wake kwa watu wetu. Tunawahubiri Habari Njema kuhusu ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu. Sisi ni wazao wao, na Mungu ameitimiza ahadi hii kwa ajili yetu. Mungu aliitimiza ahadi hii kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Tunasoma pia kuhusu hili katika Zaburi 2: ‘Wewe ni Mwanangu. Leo nimekuwa baba yako.’ Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Yesu hatarudi kaburini na kuwa mavumbi. Hivyo Mungu alisema, ‘Nitawapa ahadi ya kuaminiwa na takatifu niliyoiahidi kwa Daudi.’ Lakini Zaburi nyingine inasema, ‘Hautaruhusu Mtakatifu wako aoze kaburini.’ Daudi aliyatenda mapenzi ya Mungu alipokuwa hai. Kisha alikufa na kuzikwa kama baba zake wote. Na mwili wake ulioza kaburini! Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuoza kaburini. Ndugu zangu, eleweni yale tunayowaambia. Mnaweza kupata msamaha wa dhambi kupitia huyu Yesu. Sheria ya Musa haikuwatoa kutoka katika dhambi zenu. Lakini mnaweza kuwa huru mbali na hukumu. *** Hivyo iweni waangalifu! Msiruhusu walichosema manabii kikawatokea ninyi: ‘Sikilizeni enyi watu wenye mashaka! Mnaweza kushangaa, lakini sasa nendeni na mfe. Kwa sababu kipindi cha wakati wenu, nitafanya kitu ambacho hamtaamini. Hata kama kitafafanuliwa kwenu!’” Paulo na Barnaba walipokuwa wanaondoka kwenye sinagogi, watu waliwaomba warudi tena Sabato inayofuata ili wawaeleze zaidi kuhusu mambo haya. Baada ya mkutano, watu wengi, Wayahudi na wale waliobadili dini zao na kufuata dini ya Kiyahudi, waliwafuata Paulo na Barnaba; nao waliwatia moyo watu hawa waendelee kuitumaini neema ya Mungu. Siku ya Sabato iliyofuata, karibu watu wote katika mji walikusanyika ili wasikie neno la Bwana. Wayahudi waliokuwepo pale walipowaona watu wote hawa, wakaingiwa na wivu sana. Wakakashifu na kubishia kila kitu alichosema Paulo. Lakini Paulo na Barnaba walihubiri kwa ujasiri. Walisema, “Tulikuwa tuuhubiri ujumbe wa Mungu kwenu ninyi Wayahudi kwanza, lakini mmekataa kusikiliza. Mmeweka wazi kuwa hamstahili kuupata uzima wa milele. Hivyo tutakwenda sasa kwa wale wasio Wayahudi. Hivi ndivyo Bwana alivyotuambia kufanya: ‘Nimewafanya ninyi mwanga kwa ajili ya mataifa mengine, kuwaonesha watu ulimwenguni kote njia ya wokovu.’” Wasio Wayahudi waliposikia Paulo akisema hivi, walifurahi sana. Waliuheshimu ujumbe wa Bwana, na wengi wao wakauamini. Hawa ni wale waliochaguliwa kuupata uzima wa milele. Na hivyo ujumbe wa Bwana ulihubiriwa katika nchi yote. Lakini Wayahudi pale walisababisha baadhi ya wanawake muhimu waifuatayo dini na viongozi wa mji kuwakasirikia na kuwachukia Paulo na Barnaba na wakawafukuza mjini. Hivyo Paulo na Barnaba wakakung'uta mavumbi ya miguu yao. Kisha wakaenda katika mji wa Ikonia. Lakini wafuasi wa Bwana katika Antiokia walijaa furaha na walijazwa Roho Mtakatifu. Paulo na Barnaba walikwenda katika mji wa Ikonia. Kama walivyofanya Antiokia, waliingia katika sinagogi la Kiyahudi. Walizungumza na watu pale. Walizungumza kwa ushawishi sana kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wengi waliamini walichosema. Lakini Baadhi ya Wayahudi hawakuamini. Wayahudi hao walisema mambo yaliyowafanya wasio Wayahudi kukasirika na kuwa kinyume na waamini. Hivyo Paulo na Barnaba walikaa Ikonia kwa muda mrefu, na walihubiri kwa ujasiri kwa ajili ya Bwana. Waliwahubiri watu kuhusu neema ya Mungu. Bwana alithibitisha kwamba kile walichosema ni kweli kwa ishara na maajabu yaliyofanyika kufanyika kupitia wao. Lakini baadhi ya watu katika mji wakakubaliana na Wayahudi ambao hawakuwaamini Paulo na Barnaba. Baadhi walikubaliana na mafundisho ya mitume. Hivyo mji uligawanyika. Baadhi ya Wayahudi, viongozi wao na baadhi ya watu wasio wayahudi, walidhamiria kuwaumiza Paulo na Barnaba. Walitaka kuwaua kwa kuwapiga kwa mawe. Paulo na Barnaba walipotambua kuhusu hili, wakaondoka katika mji huo. Walikwenda Listra na Derbe, miji katika Likonia na maeneo yanayozunguka Likonia. Wakahubiri Habari Njema huko pia. Katika mji wa Listra kulikuwa mtu aliyekuwa na tatizo katika mguu wake. Alizaliwa akiwa mlemavu wa miguu na hakuwahi kutembea. Alikuwa amekaa akimsikiliza Paulo akizungumza. Paulo alipomwangalia kwa kumkazia macho alitambua kuwa mtu huyo alikuwa na imani kuwa Mungu angemponya. Hivyo Paulo akapaza sauti na kumwambia, “Simama kwa miguu yako!” Mtu yule akaruka na kuanza kutembea. Watu walipoona alichofanya Paulo, walipaza sauti kwa lugha yao wenyewe ya Kilikaonia. Walisema, “Miungu wamekuja kwetu katika maumbo ya kibinadamu!” Watu wakaanza kumwita Barnaba “Zeusi”, na Paulo “Hermesi”, kwa sababu ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu. Hekalu la Zeusi lilikuwa karibu na mji. Kuhani wa hekalu hili alileta mafahari ya ng'ombe kadhaa na mashada ya maua kwenye lango la mji. Kuhani na watu walitaka kuwatolea sadaka Paulo na Barnaba. Lakini mitume, Barnaba na Paulo walipoelewa jambo ambalo watu walikuwa wanafanya, walirarua mavazi yao. Kisha wakakimbia kuingia katikati ya watu na kuwaambia kwa kupaza sauti zao wakisema: “Ndugu, kwa nini mnafanya hivi? Sisi si miungu. Ni wanadamu kama ninyi. Tulikuja kuwaambia Habari Njema. Tunawaambia mviache vitu hivi visivyo na thamani. Mgeukieni Mungu wa kweli aishiye, aliyeumba mbingu, nchi, bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huko nyuma Mungu aliyaacha mataifa yote yatende yale waliyotaka. Lakini daima Mungu alikuwepo na alitenda mambo mema yanayothibitisha kuwa yeye ni wa hakika na wa kweli. Huwapa mvua kutoka mbinguni na mavuno bora kwa wakati sahihi. Huwapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu kwa furaha.” Hata baada Paulo na Barnaba kusema hayo, hawakuweza kuwazuia watu kuwatolea sadaka za kuteketezwa. Ndipo baadhi ya Wayahudi wakaja kutoka Antiokia na Ikonia na kuwashawishi watu ili wampinge Paulo. Hivyo wakamtupia mawe na kumburuza kumtoa nje ya mji. Wakidhani kuwa wamemwua. Lakini wafuasi wa Yesu walipokusanyika kumzunguka, aliamka na kuingia mjini. Siku iliyofuata yeye na Barnaba waliondoka na kwenda katika mji wa Derbe. Walihubiri pia Habari Njema katika mji wa Derbe, na watu wengi wakawa wafuasi wa Yesu. Kisha Paulo na Barnaba walirudi katika miji ya Listra, Ikonia na Antiokia. Katika miji hiyo waliwasaidia wafuasi kukua na kuwa na nguvu katika imani yao na waliwatia moyo kuendelea kumwamini Mungu. Waliwaambia, “Ni lazima tuteseke kwa mambo mengi katika safari yetu ya kwenda katika ufalme wa Mungu.” Waliwachagua pia wazee katika kila kanisa na kuacha kula kwa muda ili kuwaombea. Wazee hawa walikuwa wanaume wanaomtumaini Bwana Yesu, hivyo Paulo na Barnaba wakamwomba Bwana awalinde. Paulo na Barnaba walipita katikati ya eneo la Pisidia. Kisha walifika katika jimbo la Pamfilia. Waliwahubiri watu ujumbe wa Mungu katika mji wa Perge, kisha wakateremka kwenda katika mji wa Attalia. Na kutoka huko wakatweka tanga kwenda katika mji wa Antiokia ya Shamu. Huu ni mji ambako waamini waliwaweka katika uangalizi wa Mungu na kuwatuma kufanya kazi hii. Na sasa walikuwa wameimaliza. Paulo na Barnaba walipofika, walilikusanya kanisa pamoja. Waliwaambia waamini yote ambayo Mungu aliwatumia kutenda. Walisema, “Mungu amefungua mlango kwa watu wasio Wayahudi kuamini!” Na walikaa pale pamoja na wafuasi wa Bwana kwa muda mrefu. Kisha baadhi ya watu kutoka Uyahudi wakaja Antiokia na kuanza kuwafundisha jamii ya waamini wasio Wayahudi, wakisema, “Hamwezi kuokolewa ikiwa hamkutahiriwa kama Musa alivyotufundisha.” Paulo na Barnaba wakayapinga mafundisho haya na wakahojiana na kubishana na watu hawa juu ya hili. Hivyo kundi la waamini likaamua kuwatuma Paulo, Barnaba, na baadhi ya watu wengine Yerusalemu ili kujadiliana na mitume na wazee kuhusu suala hili. Kanisa liliwapa wale waliotumwa kila kitu walichohitaji kwa ajili ya safari yao. Walisafiri kupitia maeneo ya Foeniki na Samaria, ambako walieleza kwa undani mambo yote namna ambavyo wasio Wayahudi wamemgeukia Mungu wa kweli. Habari hii iliwafurahisha waamini wote. Walipofika Yerusalemu, mitume, wazee na kanisa lote waliwakaribisha. Paulo, Barnaba, na wengine wakaeleza yote ambayo Mungu alitenda kupitia wao. Baadhi ya waamini mjini Yerusalemu waliokuwa Mafarisayo, walisimama na kusema, “Waamini wasio Wayahudi lazima watahiriwe. Ni lazima tuwaambie waitii Sheria ya Musa!” Ndipo mitume na wazee wakakusanyika kulichunguza jambo hili. Baada ya majadiliano ya muda mrefu, Petro akasimama na kuwaambia, “Ndugu zangu, nina uhakika mnakumbuka kilichotokea siku za nyuma. Mungu alinichagua kutoka miongoni mwenu kuzihubiri Habari Njema kwa watu wasio Wayahudi. Kupitia mimi walisikia Habari Njema na kuamini. Mungu anamfahamu kila mtu, hata mawazo yao, na amewakubali watu hawa wasio Wayahudi. Amelionyesha hili kwetu kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi. Mbele za Mungu, wasio Wayahudi hawako tofauti na sisi. Mungu aliisafisha mioyo yao walipoamini. Kwa nini sasa mnawatwisha mzigo mzito kwenye shingo zao? Je, mnajaribu kumkasirisha Mungu? Sisi na baba zetu hatukuweza kuubeba mzigo huo. Hapana, tunaamini kuwa sisi na watu hawa tutaokolewa kwa namna moja iliyo sawa, ni kwa neema ya Bwana Yesu.” Ndipo kundi lote likawa kimya. Waliwasikiliza Paulo na Barnaba walipokuwa wanaeleza kuhusu ishara na maajabu ambayo kupitia wao Mungu aliwatendea watu wasio Wayahudi. Walipomaliza kusema, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni. Simoni Petro ametueleza namna ambavyo siku za mwanzoni Mungu alilionyesha pendo lake kwa watu wasio Wayahudi, kwa kuwakubali na kuwafanya kuwa watu wake. Maneno ya manabii yanakubaliana na hili: ‘Nitarudi baada ya hili. Nitaijenga nyumba ya Daudi tena. Imeanguka chini. Nitazijenga tena sehemu za nyumba yake zilizoangushwa chini. Nitaifanya nyumba yake kuwa mpya. Kisha wanadamu wengine wote, watu niliowachagua kutoka mataifa mengine, watataka kunifuata mimi, Bwana. Hivi ndivyo Bwana anasema, naye ndiye afanyaye mambo haya yote.’ ‘Haya yote yalijulikana tangu zamani.’ Hivyo nadhani tusiyafanye mambo kuwa magumu kwa wasio Wayahudi waliomgeukia Mungu. Badala yake, tuwatumie barua kuwaambia mambo ambayo hawapaswi kutenda: Wasile chakula kilichotolewa kwa sanamu maana chakula hiki huwa najisi. Wasijihusishe na dhambi ya zinaa. Wasile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake. Wasitende mojawapo ya mambo haya, kwa sababu bado kuna watu katika kila mji wanaofundisha Sheria ya Musa. Maneno ya Musa yamekuwa yakisomwa katika masinagogi kila siku ya Sabato kwa miaka mingi.” Mitume, wazee na kanisa lote wakataka kuwatuma baadhi ya watu wafuatane na Paulo na Barnaba kwenda Antiokia. Wakawachagua baadhi ya watu kutoka miongoni mwao wenyewe. Waliwachagua Yuda (ambaye pia aliitwa Barsaba) na Sila, watu walioheshimiwa na waamini. Kundi la waamini likaandika barua na kuwatuma watu hawa. Barua ilisema: Kutoka kwa mitume na wazee, ndugu zenu. Kwa ndugu wote wasio Wayahudi katika mji wa Antiokia na katika majimbo ya Shamu na Kilikia. Ndugu Wapendwa: Tumesikia kuwa baadhi ya watu kutoka kwetu walikuja kwenu. Walichosema kiliwasumbua na kuwaudhi. Lakini hatukuwaambia kufanya hili. Sisi sote tumekubaliana kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu. Watakuwa na rafiki zetu wapendwa, Barnaba na Paulo. Barnaba na Paulo wameyatoa maisha yao kumtumikia Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo tumewatuma Yuda na Sila pamoja nao. Watawaambia mambo yanayofanana. Imempendeza Roho Mtakatifu na sisi kwamba tusiwatwishe mizigo ya ziada, isipokuwa kwa mambo haya ya muhimu: Msile chakula kilichotolewa kwa sanamu. Msile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake. Msijihusishe na uzinzi. Mkijitenga na mambo haya, mtakuwa mnaenenda vyema. Wasalamu. Hivyo Paulo, Barnaba, Yuda, na Sila waliondoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. Walipofika huko walilikusanya kundi la waamini pamoja na wakawapa barua. Waamini walipoisoma, wakafurahi na kufarijika. Yuda na Sila ambao pia walikuwa manabii, waliwatia moyo waamini kwa maneno mengi na kuwafanya waimarike katika imani yao. Baada ya Yuda na Sila kukaa pale kwa muda, waliondoka. Waamini waliwaruhusu waende kwa amani kisha wakarudi Yerusalemu kwa wale waliowatuma. *** Lakini Paulo na Barnaba walikaa Antiokia. Wao na wengine wengi waliwafundisha waamini na kuwahubiri watu wengine Habari Njema kuhusu Bwana. Wakati fulani baadaye, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi katika miji yote tulikowahubiri watu ujumbe wa Bwana. Tuwatembelee waamini tuone wanaendeleaje.” Barnaba alitaka Yohana Marko afuatane nao pia. Lakini Yohana Marko hakukaa nao mpaka mwisho katika safari ya kwanza. Aliwaacha Pamfilia. Hivyo Paulo alisisitiza kuwa wasiende pamoja naye wakati huu. Paulo na Barnaba walikuwa na mjadala mkali kuhusu hili. Ulikuwa mbaya sana ikabidi watengane na kwenda njia tofauti. Barnaba akatweka tanga kwenda Kipro, akamchukua Marko pamoja naye. Paulo alimchagua Sila kwenda naye. Waamini Antiokia walimweka Paulo katika uangalizi wa Bwana na kumtuma. Paulo na Sila walikwenda kwa kupitia katika majimbo ya Shamu na Kilikia, wakiyasaidia makanisa kuimarika. Paulo alikwenda Derbe kisha Listra, ambako mfuasi wa Yesu aliyeitwa Timotheo aliishi. Mamaye Timotheo alikuwa mwamini wa Kiyahudi, lakini baba yake alikuwa Myunani. Waamini katika miji ya Listra na Ikonia walimsifu Timotheo kwa mambo mema. Paulo alitaka kusafiri pamoja na Timotheo, lakini Wayahudi wote walioishi katika eneo lile walijua kuwa baba yake alikuwa Myunani. Hivyo ikamlazimu Paulo amtahiri Timotheo ili kuwaridhisha Wayahudi. Kisha Paulo na wale waliokuwa pamoja naye wakasafiri kupitia miji mingine. Wakawapa waamini kanuni na maamuzi yaliyofikiwa na mitume na wazee wa Yerusalemu. Wakawaambia wazitii kanuni hizo. Hivyo makanisa yakawa yanaongezeka katika imani, na idadi ya waamini iliongezeka kila siku. Paulo na wale waliokuwa pamoja naye walisafiri kwa kupita katika maeneo ya Frigia na Galatia kwa sababu Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuzihubiri Habari Njema katika jimbo la Asia. Walipofika kwenye mpaka wa Misia, walijaribu kwenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu kwenda huko. Hivyo wakapita Misia na kwenda katika mji wa Troa. Usiku ule Paulo aliona maono kwamba mtu kutoka Makedonia alimjia Paulo. Mtu huyo alisimama mbele yake na kumsihi akisema, “Vuka njoo Makedonia utusaidie.” Baada ya Paulo kuona maono yale, tulijiandaa haraka na tukaondoka kwenda Makedonia. Tulielewa kuwa Mungu ametuita ili tukahubiri Habari Njema huko Makedonia. Tulisafiri kwa merikebu kutoka Troa na tukaabili kwenda katika kisiwa cha Samothrake. Siku iliyofuata tukasafiri kwenda katika mji wa Neapoli. Kisha tulisafiri kwa nchi kavu mpaka Filipi, koloni la Rumi na mji maarufu katika la Makedonia. Tulikaa pale kwa siku chache. Siku ya Sabato tulikwenda mtoni, nje ya lango la mji. Tulidhani tungepata mahali ambapo Wayahudi hukutana mara kwa mara kwa ajili ya kuomba. Baadhi ya wanawake walikuwa wamekusanyika huko, na hivyo tulikaa chini na kuzungumza nao. Miongoni mwao alikuwepo mwanamke aliyeitwa Lydia kutoka katika mji wa Thiatira. Alikuwa mwuza rangi ya zambarau. Alikuwa mwabudu Mungu wa kweli. Lydia alimsikiliza Paulo, na Bwana akaufungua moyo wake kuyakubali yale Paulo alikuwa anasema. Yeye na watu wote waliokuwa wakiishi katika nyumba yake walibatizwa. Kisha akatualika nyumbani mwake. Alisema, “Ikiwa mnaona mimi ni mwamini wa kweli wa Bwana Yesu, njooni mkae nyumbani mwangu.” Alitushawishi tukae nyumbani mwake. Siku moja tulipokuwa tunakwenda pale mahali pa kufanyia kuomba, mtumishi mmoja msichana alikutana nasi. Msichana huyu alikuwa na roho ya ubashiri ndani yake iliyompa uwezo wa kutabiri mambo yatakayotokea baadaye. Kwa kufanya hivi alipata fedha nyingi kwa ajili ya waliokuwa wanammiliki. Akaanza kumfuata Paulo na sisi sote kila mahali akipaza sauti na kusema, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu! Wanawaambia mnavyoweza kuokolewa!” Aliendelea kufanya hivi kwa siku kadhaa na ikamuudhi Paulo, akageuka na kumkemea yule roho akisema, “Kwa uwezo wa Yesu Kristo, ninakuamuru utoke ndani yake!” Mara ile roho chafu ikamtoka. Wamiliki wa mtumishi yule msichana walipoona hili, wakatambua kuwa hawataweza kumtumia tena ili kupata pesa. Hivyo wakawakamata Paulo na Sila na kuwaburuta mpaka kwa watawala. Wakawaleta Paulo na Sila mbele ya maofisa wa Kirumi na kusema, “Watu hawa ni Wayahudi, wanafanya vurugu katika mji wetu. Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Rumi haturuhusiwi kuzifuata wala kutenda.” Umati wote wa watu ukawa kinyume na Paulo na Sila. Maofisa wakawachania nguo Paulo na Sila na wakaamuru wapigwe bakora. Walichapwa sana kisha wakawekwa gerezani. Maofisa wakamwambia mkuu wa gereza, “Walinde watu hawa kwa umakini!” Mkuu wa gereza aliposikia amri hii maalumu, aliwaweka Paulo na Sila ndani zaidi gerezani na kuwafunga miguu yao kwenye nguzo kubwa za miti. Usiku wa manane Paulo na Sila walipokuwa wakiomba na kumwimbia Mungu nyimbo za sifa, wafungwa wengine wakiwa wanawasikiliza. Ghafla kulitokea tetemeko kubwa lililotikisa msingi wa gereza. Milango yote ya gereza ilifunguka, na minyororo waliyofungwa wafungwa wote ikadondoka. Mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza imefunguliwa. Alidhani wafungwa wametoroka, hivyo alichukua upanga wake ili ajiue. Lakini Paulo alipaza sauti akamwambia, “Usijidhuru! Sote tuko hapa!” Mkuu wa gereza akaagiza aletewe taa. Kisha akakimbia kuingia ndani, akitetemeka kwa woga, akaanguka mbele ya Paulo na Sila. Kisha akawatoa nje na kusema, “Nifanye nini ili niokoke?” Wakamwambia, “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokolewa pamoja na watu wote waishio katika nyumba yako.” Hivyo Paulo na Sila wakamhubiri ujumbe wa Bwana mkuu wa gereza na watu wote walioishi katika nyumba yake. Ilikuwa usiku sana, lakini mkuu wa gereza aliwachukua Paulo na Sila na akawaosha majeraha yao. Kisha mkuu wa gereza na watu wote katika nyumba yake wakabatizwa. Baada ya hili mkuu wa gereza akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake akawapa chakula. Watu wote walifurahi kwa sababu sasa walikuwa wanamwamini Mungu. Asubuhi iliyofuata maofisa wa Kirumi waliwatuma baadhi ya askari kwenda gerezani na wakamwambia mkuu wa gereza, “Waachie watu hawa huru.” Mkuu wa gereza akamwambia Paulo, “Maofisa wamewatuma askari hawa ili kuwaachia huru. Mnaweza kuondoka sasa. Nendeni kwa amani.” Lakini Paulo akawaambia askari, “Wale maofisa hawakuthibitisha kuwa tulifanya chochote kibaya, lakini walitupiga kwa bakora hadharani na kutuweka gerezani. Nasi ni raia wa Rumi. Na sasa wanataka tuondoke kimya kimya. Haiwezekani, ni lazima waje hapa wao wenyewe kisha watutoe nje!” Askari wakawaambia maofisa alichosema Paulo. Waliposikia kwamba Paulo na Sila ni raia wa Rumi, waliogopa. Hivyo walikwenda gerezani kuwaomba msamaha. Waliwatoa nje ya gereza na kuwaomba waondoke mjini. Lakini Paulo na Sila walipotoka gerezani, walikwenda nyumbani kwa Lydia. Wakawaona baadhi ya waamini pale, wakawatia moyo. Kisha wakaondoka. Paulo na Sila walisafiri kupitia miji ya Amfipoli na Apolonia. Wakafika katika mji wa Thesalonike, ambako kulikuwa sinagogi la Kiyahudi. Paulo aliingia katika sinagogi kuwaona Wayahudi kama alivyokuwa akifanya. Wiki tatu zilizofuatia, kila siku ya Sabato alijadiliana nao kuhusu Maandiko. Alifafanua Maandiko kuwaonesha kuwa Masihi ilikuwa afe na kufufuka kutoka kwa wafu. Aliwaambia, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake ndiye Masihi.” Baadhi ya Wayahudi pale waliwaamini Paulo na Sila na waliamua kujiunga nao. Idadi kubwa ya Wayunani waliokuwa wanamwabudu Mungu wa kweli na wanawake wengi maarufu walijiunga nao pia. Lakini Wayahudi ambao hawakuamini wakaingiwa na wivu, hivyo wakawakusanya baadhi ya watu wabaya katikati ya mji ili kufanya vurugu. Wakaunda kundi na wakanzisha vurugu mjini. Walikwenda nyumbani kwa Yasoni kuwatafuta Paulo na Sila. Walitaka kuwaleta mbele ya watu. Walipowakosa wakamkamata na kumburuta Yasoni na baadhi ya waamini wengine na kuwapeleka kwa viongozi wa mji. Watu wakapasa sauti na kusema, “Watu hawa Wamesababisha matatizo mengi kila mahali ulimwenguni, na sasa wamekuja hapa pia! Yasoni amewaweka nyumbani mwake. Wanavunja sheria za Kaisari. Wanasema kuna mfalme mwingine anayeitwa Yesu.” Viongozi wa mji na watu wengine waliposikia hili waliudhika sana. Wakawalazimisha Yasoni na waamini wengine kuweka dhamana ya fedha kuthibitisha kuwa hakutakuwa vurugu tena. Kisha wakawaruhusu kuondoka. Usiku ule ule waamini wakawapeleka Paulo na Sila katika mji mwingine ulioitwa Berea. Walipofika pale, walikwenda katika sinagogi la Kiyahudi. Watu wa Berea walikuwa radhi kujifunza kuliko watu wa Thesalonike. Walifurahi waliposikia ujumbe aliowaambia Paulo. Waliyachunguza Maandiko kila siku ili kuhakikisha kuwa waliyoyasikia ni ya kweli. Matokeo yake ni kuwa watu wengi miongoni mwao waliamini, wakiwemo wanawake maarufu Wayunani na wanaume. Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipojua kuwa Paulo alikuwa anawahubiri Ujumbe wa Mungu katika mji wa Berea, walikwenda huko pia. Waliwakasirisha watu na kufanya vurugu. Hivyo waamini walimpeleka Paulo sehemu za pwani, lakini Sila na Timotheo walibaki Berea. Wale waliokwenda na Paulo walimpeleka katika mji wa Athene. Waliporudi Berea, waliwapa ujumbe kutoka kwa Paulo Timotheo na Sila kuwa waende kuungana naye haraka kadiri watakavyoweza. Paulo alipokuwa akiwasubiri Sila na Timotheo katika mji wa Athene, aliudhika kwa sababu aliona mji ulikuwa umejaa sanamu. Alipokuwa katika sinagogi alizungumza na Wayahudi na Wayunani waliokuwa wakimwabudu Mungu wa kweli. Alikwenda pia katika sehemu za wazi za umma za mikutano na kuzungumza na kila aliyekutana naye. Baadhi ya wanafalsafa Waepikureo na baadhi ya wanafalsafa Wastoiko walibishana naye. Baadhi yao walisema, “Mtu huyu hakika hajui anachokisema. Anajaribu kusema nini?” Paulo alikuwa anawaambia Habari Njema kuhusu Yesu na ufufuo. Hivyo walisema, “Anaonekana anatueleza kuhusu baadhi ya miungu wa kigeni.” Walimchukua Paulo kwenye mkutano wa baraza la Areopago. Wakasema, “Tafadhali tufafanunile hili wazo jipya ambalo umekuwa ukifundisha. Mambo unayosema ni mapya kwetu. Hatujawahi kusikia mafundisho haya, na tunataka kufahamu yana maana gani.” (Watu wa Athene na wageni walioishi pale walitumia muda wao bila kufanya kazi yoyote isipokuwa kusikiliza na kuzungumza kuhusu mawazo mapya.) Ndipo Paulo alisimama mbele ya mkutano wa baraza la Areopago na kusema, “Watu wa Athene, kila kitu ninachokiona hapa kinanionyesha kuwa ninyi ni watu wa dini sana. Nilikuwa natembea katika mji wenu na nimeona mambo mnayoyaabudu. Niliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya juu yake: ‘KWA MUNGU ASIYEJULIKANA.’ Mnamwabudu mungu msiyemjua. Huyu ni Mungu ninayetaka kuwaambia habari zake. Ni Mungu aliyeumba ulimwengu na kila kitu ndani yake. Ni Bwana wa mbingu na nchi. Haishi katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya kibinadamu. Ndiye anayewapa watu uzima, pumzi na kila kitu wanachohitaji. Hahitaji msaada wowote kutoka kwao. Ana kila kitu anachohitaji. Mungu alianza kwa kumwumba mtu mmoja, na kutoka kwake aliumba mataifa yote mbalimbali, na akawaweka kila mahali ulimwenguni. Na aliamua ni wakati gani na wapi ambapo angewaweka ili waishi. Mungu alitaka watu wamtafute yeye, na pengine kwa kumtafuta kila mahali, wangempata. Lakini hayuko mbali na kila mmoja wetu. Ni kupitia Yeye tunaweza kuishi, kufanya yale tunayofanya na kuwa kama tulivyo. Kama baadhi ya methali zenu zilivyokwisha sema, ‘Sote tunatokana naye.’ Huo ndio ukweli. Sote tunatokana na Mungu. Hivyo ni lazima msifikiri kuwa Yeye ni kama kitu ambacho watu hukidhania au kukitengeneza. Hivyo ni lazima tusifikiri kuwa ametengenezwa kwa dhahabu, fedha au jiwe. Hapo zamani watu hawakumwelewa Mungu, naye Mungu hakulijali hili. Lakini sasa anawaagiza wanadamu kila mahali kubadilika na kumgeukia Yeye. Amekwisha chagua siku ambayo atawahukumu watu wote ulimwenguni katika namna isiyo na upendeleo. Atafanya hili kwa kumtumia mtu aliyemchagua zamani zilizopita. Na alithibitisha kwa kila mtu kwamba huyu ndiye mtu atakayefanya. Alilithibitisha kwa kumfufua kutoka kwa wafu!” Watu waliposikia kuhusu mtu kufufuliwa kutoka kwa kifo, baadhi yao walicheka. Lakini wengine walisema, “Tutasikiliza mengi kuhusu hili kutoka kwako baadaye.” Hivyo Paulo akaondoka kwenye mkutano wa baraza. Lakini baadhi ya watu waliungana na Paulo na kuwa waamini. Miongoni mwao walikuwa Dionisi, ambaye alikuwa mjumbe wa baraza la Areopago, na mwanamke aliyeitwa Damari na baadhi ya wengine. Baadaye, Paulo aliondoka Athene na kwenda katika mji wa Korintho. Akiwa huko alikutana na Myahudi aliyeitwa Akila, aliyezaliwa katika jimbo la Ponto. Lakini yeye na mke wake aliyeitwa Prisila, walikuwa tu ndiyo wamehamia Korintho kutoka Italia. Waliondoka Italia kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ametoa amri Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo alikwenda kuwatembelea Akila na Prisila. Walikuwa watengenezaji wa mahema, kama alivyokuwa Paulo, hivyo alikaa na kufanya kazi pamoja nao. Kila siku ya Sabato Paulo alikwenda kwenye sinagogi na kuzungumza na Wayahudi na Wayunani, akijaribu kuwashawishi wamwamini Yesu. Lakini baada ya Sila na Timotheo kufika kutoka Makedonia, Paulo alitumia muda wake wote kuuhubiri ujumbe wa Mungu kwa Wayahudi, akiwaeleza kuwa Yesu ndiye Masihi. Lakini walimpinga Paulo na wakaanza kumtukana. Hivyo Paulo akakung'uta mavumbi kutoka kwenye nguo zake. Akawaambia, “Msipookolewa, itakuwa makosa yenu ninyi wenyewe! Nimefanya yote ninayoweza kufanya. Baada ya hili nitawaendea watu wasio Wayahudi tu.” Paulo aliondoka katika sinagogi na kuhamia nyumbani kwa Tito Yusto, mtu aliyekuwa anamwabudu Mungu wa Kweli, nyumba yake ilikuwa jirani na sinagogi. Krispo aliyekuwa kiongozi wa sinagogi lile, pamoja na watu wote waliokuwa wanaishi nyumbani mwake walimwamini Bwana Yesu. Watu wengi katika mji wa Korintho walimsikiliza Paulo, wakaamini na wakabatizwa. Wakati wa usiku, Paulo aliona maono. Bwana alimwambia, “Usiogope, na usiache kuzungumza na watu. Niko pamoja nawe, na hakuna atakayeweza kukudhuru. Kuna watu wangu wengi katika mji huu.” Paulo alikaa pale kwa mwaka mmoja na nusu akiwafundisha watu ujumbe wa Mungu. Galio alipokuwa gavana wa Akaya, baadhi ya Wayahudi walikusanyika wakawa kinyume cha Paulo. Wakampeleka mahakamani. Wakamwambia Galio, “Mtu huyu anawafundisha watu kumwabudu Mungu kwa namna ambavyo ni kunyume na sheria yetu!” Paulo alikuwa tayari kuzungumza, lakini Galio aliwaambia Wayahudi, “Ningewasikiliza ikiwa malalamiko yenu yangehusu dhuluma au kosa jingine. Lakini yanahusu maneno na majina tu, mabishano yanayohusu sheria zenu wenyewe. Ni lazima mtatue tatizo hili ninyi wenyewe. Sitaki kuwa mwamuzi wa jambo hili.” Hivyo Galio akawafanya waondoke mahakamani. Kisha wote kwa pamoja wakamkamata Sosthenesi, kiongozi wa sinagogi. Wakampiga mbele ya mahakama. Lakini Galio hakulijali hili pia. Paulo alikaa na waamini kwa siku nyingi. Kisha aliondoka na kusafiri majini kwenda Shamu. Prisila na Akila walikuwa pamoja naye pia. Walipofika Kenkrea Paulo akanyoa nywele zake kwa sababu aliweka nadhiri kwa Mungu. Kisha walikwenda Efeso, ambako Paulo aliwaacha Prisila na Akila. Paulo alipokuwa Efeso alikwenda katika sinagogi na kuzungumza na Wayahudi. Walimwomba akae kwa muda mrefu lakini alikataa. Aliwaacha na kusema, “Nitarudi tena kwenu ikiwa Mungu atataka nirudi.” Na hivyo akaabili kwenda Efeso. Alipofika Kaisaria, alikwenda Yerusalemu na kulitembelea kanisa pale. Baada ya hapo alikwenda Antiokia. Alikaa Antiokia kwa muda kisha akaondoka akipita katika nchi za Galatia na Frigia. Alisafiri kutoka mji mmoja hadi mji mwingine katika mikoa hii, akiwasaidia wafuasi wa Yesu kuimarika katika imani yao. Myahudi aliyeitwa Apolo alikuja Efeso. Alizaliwa katika mji wa Iskanderia, alikuwa msomi aliyeyajua Maandiko vizuri. Alikuwa amefundishwa kuhusu Bwana na daima alifurahia kuwaeleza watu kuhusu Yesu. Alichofundisha kilikuwa sahihi, lakini ubatizo alioufahamu ni ubatizo aliofundisha Yohana. Apolo alianza kuzungumza kwa ujasiri katika sinagogi. Prisila na Akila walipomsikia akizungumza, walimchukua wakaenda naye nyumbani mwao kisha wakamsaidia kuielewa njia ya Mungu vizuri zaidi. Apolo alitaka kwenda Akaya. Hivyo waamini wa Efeso wakamsaidia. Waliwaandikia barua wafuasi wa Bwana waliokuwa Akaya wakiwaomba wampokee Apolo. Alipofika pale, alikuwa msaada mkubwa kwa wale waliomwamini Yesu kwa sababu ya neema ya Mungu. Alibishana kwa ujasiri na Wayahudi mbele ya watu wote. Alithibitisha kwa uwazi kuwa wayahudi walikuwa wanakosea. Alitumia Maandiko kuonesha kuwa Yesu ndiye Masihi. Apolo alipokuwa katika mji wa Korintho, Paulo alikuwa anatembelea baadhi ya sehemu akiwa njiani kwenda Efeso. Alipofika Efeso waliwakuta baadhi ya wafuasi wa Bwana. Akawauliza, “Mlimpokea Roho Mtakatifu mlipoamini?” Wafuasi hao wakamwambia, “Hatujawahi hata kusikia kuhusu Roho Mtakatifu!” Paulo akawauliza, “Kwa hiyo ni mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakasema, “Kwa ubatizo aliofundisha Yohana.” Paulo akasema, “Yohana aliwaambia watu wabatizwe kuonesha kuwa walidhamiria kubadili maisha yao. Aliwaambia watu kuamini katika yule atakaye kuja baada yake, naye huyo ni Yesu.” Wafuasi hawa waliposikia hili, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. Kisha Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akaja juu yao. Wakaanza kuzungumza na kutabiri katika lugha tofauti. Walikuwepo wanaume kama kumi na mbili katika kundi hili. Paulo akaingia katika sinagogi na akazungumza kwa ujasiri. Aliendelea kufanya hivi kwa miezi mitatu. Alizungumza na Wayahudi, akijaribu kuwashawishi kukubali alichokuwa anawaambia kuhusu ufalme wa Mungu. Lakini baadhi yao wakawa wakaidi, wakakataa kuamini. Waliikashifu Njia ya Bwana mbele ya kila mtu. Hivyo Paulo aliwaacha Wayahudi hawa na kuwachukua wafuasi wa Bwana pamoja naye. Alikwenda mahali ambapo mtu aitwaye Tirano alikuwa na shule. Hapo Paulo alizungumza na watu kila siku. Alifanya hivi kwa miaka miwili na kila mtu aliyeishi Asia, Wayahudi na Wayunani alilisikia neno la Bwana. Mungu alimtumia Paulo kufanya miujiza ya kipekee. Baadhi ya watu walichukua vitambaa vya mkononi na nguo zilizovaliwa na Paulo na kuziweka juu ya wagonjwa. Wagonjwa waliponywa na pepo wabaya waliwatoka watu. Pia baadhi ya Wayahudi walikuwa wanasafiri huku na huko wakiwatoa pepo wabaya kwa watu. Wana saba wa Skewa, mmoja wa viongozi wa makuhani, walikuwa wakifanya hili. Wayahudi hawa walijaribu kutumia jina la Bwana kuyatoa mapepo kwa watu. Wote walikuwa wanasema, “Katika jina la Bwana Yesu anayezungumzwa na Paulo ninakuamuru utoke!” *** Lakini wakati fulani pepo akawaambia Wayahudi hawa, “Ninamfahamu Yesu, na ninafahamu kuhusu Paulo, na ninyi ni nani?” Kisha mtu aliyekuwa na pepo ndani yake akawarukia. Alikuwa na nguvu kuliko wote. Akawapiga, akawachania nguo za na kuwavua, nao wakakimbia kutoka katika nyumba ile wakiwa uchi. Watu wote katika Efeso, Wayahudi na Wayunani wakafahamu kuhusu hili. Wakaogopa na kumtukuza Bwana Yesu. Waamini wengi walianza kukiri, wakisema mambo yote maovu waliyotenda. Baadhi yao walikuwa wametumia uchawi huko nyuma. Waamini hawa walileta vitabu vyao vya uchawi na kuvichoma mbele ya kila mtu. Vitabu hivi vilikuwa na thamani ya sarafu hamsini elfu za fedha. Hivi ndivyo ambavyo neno la Bwana lilikuwa linasambaa kwa nguvu, likisababisha watu wengi kuamini. Baada ya hili, Paulo alipanga kwenda Yerusalemu. Alipanga kupitia katika majimbo ya Makedonia na Akaya kisha kwenda Yerusalemu. Alisema, “Baada ya kwenda Yerusalemu, ni lazima niende Rumi pia.” Timotheo na Erasto walikuwa wasaidizi wake wawili. Paulo aliwatuma watangulie Makedonia. Lakini yeye alikaa Asia kwa muda. Lakini katika wakati huo huo kulikuwepo tatizo kuhusiana na Njia. Hivi ndivyo ilivyotokea: Alikuwepo mtu aliyeitwa Demetrio aliyekuwa mfua fedha. Alikuwa akitengeneza sanamu ndogo za fedha zilizofanana na hekalu la Artemi, mungu mke. Wanaume waliokuwa wakifanya kazi hii walijipatia pesa nyingi sana. Demetrio alifanya mkutano na watu hawa pamoja na wengine waliokuwa wanafanya kazi ya aina hiyo. Akawaambia, “Ndugu, mnafahamu kuwa tunapata pesa nyingi kutokana na kazi yetu. Lakini angalieni kitu ambacho mtu huyu Paulo anafanya. Sikilizeni anachosema. Amewashawishi watu wengi katika Efeso na karibu Asia yote kubadili dini zao. Anasema miungu ambayo watu wanatengeneza kwa mikono si miungu wa kweli. Ninaogopa hili litawafanya watu kuwa kinyume na biashara yetu. Lakini kuna tatizo jingine pia. Watu wataanza kufikiri kuwa hekalu la Artemi, mungu wetu mkuu halina maana. Ukuu wake utaharibiwa. Na Artemi ni mungu mke anayeabudiwa na kila mtu katika Asia na ulimwengu wote.” Waliposikia hili, walikasirika sana. Wakapaza sauti zao wakisema, “Artemi, mungu mke wa Efeso ni mkuu!” Mji wote ukalipuka kwa vurugu. Watu wakawakamata Gayo na Aristarko, waliotoka Makedonia waliokuwa wanasafiri na Paulo, wakawapeleka kwenye uwanja wa mji. Paulo alitaka kwenda ili azungumze na watu, lakini wafuasi wa Bwana walimzuia. Pia, baadhi ya viongozi katika jimbo la Asia waliokuwa rafiki zake walimtumia ujumbe wakimwambia asiende uwanjani. Watu wengi walikuwa akipiga kelele kusema hili na wengine walisema jambo jingine. Mkutano ukawa na vurugu kubwa. Watu wengi hawakujua ni kwa nini walikwenda pale. Baadhi ya Wayahudi wakamshawishi mtu mmoja aliyeitwa Iskanda asimame mbele ya umati, wakamwelekeza cha kusema. Iskanda alipunga mkono wake, akijaribu kuwaeleza watu jambo. Lakini watu walipoona kuwa Iskanda ni Myahudi, wote wakaanza kupiga kelele ya aina moja. Kwa masaa mawili waliendelea kusema, “Artemi, mungu mke wa Efeso ni mkuu!” Ndipo karani wa mji akawashawishi watu kunyamaza. Akawaambia, “Watu wa Efeso, kila mtu anafahamu kwamba Efeso ndiyo mji unaotunza hekalu la mungu mkuu mke Artemi. Kila mtu anafahamu pia kwamba tunatunza mwamba wake mtakatifu. Hakuna anayeweza kupinga hili, hivyo mnyamaze. Ni lazima mtulie na kufikiri kabla hamjafanya kitu chochote. Mmewaleta watu hawa hapa, lakini hawajasema kitu chochote kibaya kinyume na mungu wetu mke. Hawajaiba kitu chochote kutoka kwenye hekalu lake. Tuna mahakama za sheria na wapo waamuzi. Je, Demetrio na watu hawa wanaofanya kazi pamoja naye wana mashitaka dhidi ya yeyote? Wanapaswa kwenda mahakamani wakawashtaki huko. Kuna kitu kingine mnataka kuzungumzia? Basi njooni kwenye mikutano ya kawaida ya mji mbele ya watu. Litaweza kuamuriwa huko. Ninasema hivi kwa sababu mtu mwingine anaweza kuona tukio hili la leo na akatushtaki kwa kuanzisha ghasia. Hatutaweza kufafanua vurugu hii, kwa sababu hakuna sababu za msingi za kuwepo mkutano huu.” Baada ya karani wa mji kusema hili, aliwaambia watu kwenda majumbani mwao. Ghasia zilipokwisha, Paulo aliwaalika wafuasi wa Bwana kuja kumtembelea. Baada ya kuwatia moyo, aliwaaga na kuondoka kwenda Makedonia. Katika safari yake kupitia Makedonia alikuwa na maneno mengi ya kuwatia moyo wafuasi sehemu mbalimbali. Kisha alikwenda Uyunani na alikaa huko kwa miezi mitatu. Alipokuwa tayari kutweka tanga kwenda Shamu, baadhi ya Wayahudi walikuwa wanapanga kitu kinyume naye. Hivyo aliamua kurudi nyuma kwenda Shamu kupitia Makedonia. Watu hawa walikuwa wanasafiri pamoja naye: Sopata, mwana wa Piro, kutoka mji wa Berea; Aristarko na Sekundo, kutoka mji wa Thesalonike; Gayo, kutoka mji wa Derbe; Timotheo; na watu wawili kutoka Asia, Tikiko na Trofimo. Watu hawa walimtangulia Paulo. Walitusubiri katika mji wa Troa. Baada ya Siku kuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu tulitweka tanga kutoka katika mji wa Filipi. Tuliwakuta watu hawa katika mji wa Troa siku tano baadaye na tulikaa pale kwa siku saba. Siku ya Jumapili sote tulikusanyika pamoja kula Meza ya Bwana. Paulo alizungumza na kundi. Kwa sababu alipanga kuondoka siku iliyofuata, aliendelea kuzungumza mpaka usiku wa manane. Tulikuwa wote kwenye chumba ghorofani na kulikuwa taa nyingi chumbani. Alikuwepo kijana mmoja aliyekuwa amekaa dirishani aliyeitwa Eutiko. Paulo aliendelea kuzungumza, na Eutiko alianza kuchoka na kusikia ungungizi. Mwishowe alisinzia na kuanguka. Alianguka chini, nje kutoka ghorofa ya tatu. Watu walipokwenda kumnyenyua alikuwa amekwisha kufa. Paulo alishuka, akaenda mahali alipokuwa Eutiko, akapiga magoti, na akamkumbatia. Akawaambia waamini wengine, “Msiwe na hofu. Ni mzima yuko hai sasa.” Kisha Paulo akapanda ghorofani, akamega baadhi ya mikate na kula. Alizungumza nao kwa muda mrefu. Alimaliza kuzungumza mapema asubuhi na akaondoka. Wafuasi wa Bwana walimpeleka Eutiko nyumbani akiwa hai, walifarijika sana wote. Tulimtangulia Paulo, tukatweka tanga kwenda Asso, tulipanga kumkuta huko. Alitwambia tufanye hivi kwa sababu alitaka kusafiri kwa nchi kavu. Alipotukuta Asso, aliungana nasi na tulipanda meli pamoja naye, na sote tulitweka tanga kwenda Mitelene. Siku iliyofuata, tulitweka tanga kutoka pale na kufika karibu na kisiwa cha Kio. Kisha siku iliyofuata tulitweka tanga kwenda kwenye kisiwa Samosi. Baada ya siku moja tukafika kwenye mji wa Mileto. Paulo alikwisha amua kutosimama Efeso. Hakutaka kukaa Asia kwa muda mrefu. Alikuwa anaharakisha kwa sababu alitaka ikiwezekana awe Yerusalemu siku ya Pentekoste. Tukiwa Mileto Paulo alitume ujumbe kwenda Efeso, akiwaambia wazee wa kanisa la Efeso waje kwake. Walipofika, Paulo akawaambia, “Mnafahamu kuhusu maisha yangu tangu siku ya kwanza nilipofika Asia. Mnafahamu namna nilivyoishi wakati wote nilipokuwa pamoja nanyi. Wayahudi walipanga hila kinyume nami, na hila zao zilinisababishia matatizo mengi. Lakini mnafahamu kwamba daima nilimtumikia Bwana, nyakati zingine kwa machozi. Sikujipendelea mimi mwenyewe kwanza. Daima niliwatendea mema. Niliwahubiri Habari Njema kuhusu Yesu sehemu za wazi mbele ya watu na pia nilifundisha katika nyumba zenu. Nilimwambia kila mtu, Myahudi na Myunani, kubadilika na wakamgeukia Mungu. Niliwaambia wote wamwamini Bwana wetu Yesu. Lakini sasa ni lazima nimtii Roho na kwenda Yerusalemu. Sifahamu nini kitanipata huko. Ninafahamu kitu kimoja kwamba katika kila mji Roho Mtakatifu huniambia kwamba matatizo na hata kufungwa gerezani kunanisubiri. Siujali uhai wangu mwenyewe. Jambo la muhimu zaidi ni mimi kuimaliza kazi yangu. Ninataka niimalize huduma ambayo Bwana Yesu alinipa niifanye, nayo ni kuwahubiri watu Habari Njema kuhusu neema ya Mungu. Na sasa nisikilizeni. Ninafahamu kwamba hakuna mmoja wenu atakayeniona tena. Wakati wote nilipokuwa pamoja nanyi, niliwahubiri Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Hivyo leo ninaweza kuwaambia kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho: Mungu hatanilaumu ikiwa baadhi yenu hamtaokoka. Ninaweza kusema hivi kwa sababu ninajua niliwaambia yote ambayo Mungu anataka mfahamu. Jilindeni ninyi wenyewe pamoja na watu wote mliopewa na Mungu. Naye Roho Mtakatifu amewapa ninyi kazi ya kuwachunga kondoo hawa. Ni lazima muwe wachungaji wa kanisa la Mungu, watu ambao Mungu aliwanunua kwa damu ya Mwanaye wa pekee. Ninafahamu ya kwamba nikishaondoka, baadhi ya watu watakuja kwenye kundi letu. Watakuwa kama mbwa mwitu na watajaribu kuwaangamiza kondoo. Pia, watu kutoka kwenye kundi lenu wenyewe wataanza kufundisha mambo yasiyo sahihi. Watawaongoza baadhi ya wafuasi wa Bwana mbali na kweli ili wawafuate katika upotovu wao. Hivyo iweni waangalifu! Na daima kumbukeni mambo niliyofanya kwa miaka mitatu nilipokuwa pamoja nanyi. Sikuacha kumkumbusha kila mmoja wenu jinsi anavyopaswa kuishi, nikiwashauri usiku na mchana na kulia kwa ajili yenu. Sasa ninawaweka katika uangalizi wa Mungu. Ninategemea ujumbe wa neema yake kuwaimarisha ninyi. Ujumbe huo unaweza kuwapa ninyi baraka ambazo Mungu huwapa watakatifu wake wote. Nilipokuwa pamoja nanyi, sikutamani pesa ya mtu yeyote au nguo nzuri. Mnafahamu kwamba daima nilifanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe ili nimudu mahitaji yangu mwenyewe na mahitaji ya watu waliokuwa pamoja nami. Daima niliwaonesha kwamba mnapaswa kufanya kazi nilivyofanya na kuwasaidia wadhaifu. Niliwafundisha kukumbuka maneno ya Bwana Yesu aliyosema, ‘Ni baraka kuu kutoa kuliko kupokea.’” Paulo alipomaliza kuzungumza, alipiga magoti chini, na wote waliomba pamoja. Walilia sana. Kilichowahuzunisha sana ilikuwa kauli ya Paulo alipowaambia kuwa hawatamwona tena. Walimkumbatia na kumbusu. Kisha walikwenda pamoja naye mpaka kwenye meli na wakaagana naye. Baada ya kuwaaga wazee tulitweka tanga moja kwa moja kwenda kwenye kisiwa cha Kosi. Siku iliyofuata tulikwenda kisiwa cha Rhode na kutoka pale tulikwenda Patara. Tulipata meli hapo iliyokuwa inakwenda maeneo ya Foeniki. Tukapanda meli na tukatweka tanga kuondoka. Tulitweka tanga na kusafiri karibu na kisiwa cha Kipro. Tuliweza kukiona upande wa kaskazini, lakini hatukusimama. Tulisafiri mpaka katika jimbo la Shamu. Tulisimama Tiro kwa sababu meli ilitakiwa kupakua mizigo yake pale. Tuliwapata wafuasi wa Bwana pale na tukakaa pamoja nao kwa siku saba. Walimuonya Paulo asiende Yerusalemu kwa sababu ya kile walichoambiwa na Roho Mtakatifu. Lakini muda wetu wa kukaa pale ulipokwisha, tulirudi kwenye meli na kuendelea na safari yetu. Wafuasi wote, hata wanawake na watoto walikuja pamoja nasi pwani. Tulipiga magoti ufukweni sote, tukaomba, na tukaagana. Kisha tukaingia melini, na wafuasi wa Bwana wakarudi nyumbani. Tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro na kwenda katika mji wa Ptolemai. Tuliwasalimu waamini pale na kukaa nao kwa siku moja. Siku iliyofuata tuliondoka Ptolemai na kwenda katika mji wa Kaisaria. Tulikwenda nyumbani kwa Filipo na kukaa kwake, alikuwa mhubiri wa Habari Njema. Alikuwa mmoja wa wasaidizi saba. Alikuwa na mabinti wanne mabikira waliokuwa na karama ya kutabiri. Baada ya kuwa pale kwa siku kadhaa, nabii aliyeitwa Agabo alikuja kutoka Uyahudi. Alikuja Kwetu na kuazima mkanda wa Paulo. Aliutumia mkanda huo na akajifunga mikono na miguu yake mwenyewe. Kisha akasema, “Roho Mtakatifu ananiambia, ‘Hivi ndivyo ambavyo Wayahudi walioko Yerusalemu watamfunga mtu anayeuvaa mkanda huu. Kisha watamkabidhi kwa watu wasiomjua Mungu.’” Tuliposikia hili, sisi na wafuasi wengine pale tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu. Lakini Paulo alisema, “Kwa nini mnalia na kunihuzunisha? Niko radhi kufungwa Yerusalemu. Niko tayari hata kufa kwa ajili ya jina la Bwana Yesu!” Hatukuweza kumshawishi asiende Yerusalemu. Hivyo tuliacha kumsihi na tukasema, “Tunaomba lile alitakalo Bwana lifanyike.” Baada ya hili, tulijiandaa na kuelekea Yerusalemu. Baadhi ya Wafuasi wa Yesu kutoka Kaisaria walikwenda pamoja nasi. Wafuasi hawa walitupeleka nyumbani kwa Mnasoni, mtu kutoka Kipro, ambaye alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kuwa wafuasi wa Yesu. Walitupeleka nyumbani kwake ili tukae pamoja naye. Ndugu na dada wa Yerusalemu walitukabisha kwa furaha sana walipotuona. Siku iliyofuata Paulo alikwenda pamoja nasi kumtembelea Yakobo. Wazee wote walikuwepo pia. Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwaambia hatua kwa hatua yote ambayo Mungu aliyatenda katikati ya watu wasio Wayahudi kupitia huduma yake. Viongozi waliposikia hili, wakamsifu Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, “Ndugu yetu, unaweza kuona maelfu ya Wayahudi wamekuwa waamini, lakini wanadhani ni muhimu kutii Sheria ya Musa. Wameambiwa kuwa unawafundisha Wayahudi wanaoishi katika majimbo yasiyo ya Kiyahudi kuacha kufuata Sheria ya Musa. Wamesikia kuwa unawaambia wasiwatahiri watoto wao na wasifuate desturi zetu. Tufanye nini? Wafuasi wayahudi hapa watajua kuwa umekuja. Hivyo tutakwambia nini cha kufanya: Watu wanne miongoni mwa watu wetu wameweka nadhiri kwa Mungu. Wachukue watu hawa walio pamoja nawe na ushiriki katika ibada ya utakaso. Lipia gharama zao ili wanyoe nywele za vichwa vyao. Hili litathibitisha kwa kila mmoja kuwa mambo waliyosikia kuhusu wewe si sahihi. Watajua kuwa wewe mwenyewe unaitii Sheria ya Musa katika maisha yako. Tumekwisha watumia barua waamini wasio Wayahudi kuwaambia ambayo hawapaswi kufanya: ‘Wasile chakula kilichotolewa kwa sanamu. Wasile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama zilizo na damu ndani yake. Wasijihusishe na uzinzi.’” Hivyo Paulo akawachukua wale watu wanne aliokuwa pamoja nao. Siku iliyofuata alishiriki kwenye ibada ya kuwatakasa. Kisha akaenda eneo la Hekalu na kutangaza siku ya mwisho ambapo kipindi cha utakaso kitakwisha na kwamba sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wa watu hao siku hiyo. Siku saba zilipokuwa zinakaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka Asia walimwona Paulo katika eneo la Hekalu. Wakamshawishi kila mtu, kisha wakakusanyika kama kundi wakiwa na hasira, kisha wakamkamata Paulo na wakapiga kelele wakisema, “Watu wa Israeli, tusaidieni! Huyu ndiye mtu anayefundisha mambo yaliyo kinyume na Sheria ya Musa, kinyume na watu wetu, na kinyume na Hekalu letu. Hivi ndivyo anavyowafundisha watu kila mahali. Na sasa amewaleta baadhi ya Wayunani katika eneo la Hekalu na amepanajisi mahali hapa patakatifu!” (Wayahudi walisema hili kwa kuwa walimwona Trofimo akiwa na Paulo Yerusalemu. Trofimo alikuwa mwenyeji wa Efeso, Wayahudi walidhani kuwa Paulo alikuwa amempeleka eneo takatifu la Hekalu.) Watu katika mji wote wakajaa hasira, na kila mtu akaja akikimbilia kwenye Hekalu. Wakamkamata Paulo na kumtoa nje ya eneo takatifu, malango ya Hekalu yakafungwa saa hiyo hiyo. Walipokuwa wanajaribu kumwua Paulo, Kamanda wa jeshi la Rumi katika mji wa Yerusalemu akapata taarifa kuwa ghasia zilikuwa zimeenea mji wote. Mara hiyo hiyo kamanda alikimbilia mahali ambako umati wa watu ulikuwa umekusanyika, aliwachukua baadhi ya maofisa wa jeshi na askari. Watu walipomwona kamanda na askari wake waliacha kumpiga Paulo. Kamanda alikwenda mahali alipokuwa Paulo na akamkamata. Akawaambia askari wake wamfunge kwa minyororo miwili. Kisha akauliza, “Mtu huyu ni nani? Amefanya nini kibaya?” Baadhi ya watu pale walipiga kelele wakisema kitu hiki na wengine walisema kingine. Kwa sababu ya kuchanganyikiwa huku na kelele kamanda hakujua ukweli kuhusu kilichotokea. Hivyo akawaambia askari wamchukue Paulo mpaka kwenye jengo la jeshi. Umati wote ulikuwa unawafuata. Askari walipofika kwenye ngazi ilibidi wambebe Paulo. Walifanya hivi ili kumlinda, kwa sababu watu walikuwa tayari kumwumiza. Watu walikuwa wanapiga kelele wakisema, “Auawe!” *** Askari walipokuwa tayari kumwingiza Paulo kwenye jengo la jeshi, Paulo alimwuliza kamanda akasema, “Je, ninaweza kukwambia kitu?” Kamanda akasema, “Kumbe, unaongea Kiyunani? Kwa hiyo wewe si mtu niliyemdhania. Nilidhani wewe ni Mmisri aliyeanzisha vurugu dhidi ya serikali siku si nyingi na akawaongoza magaidi elfu nne kwenda jangwani.” Paulo akasema, “Hapana, Mimi ni Myahudi kutoka Tarso katika jimbo la Kilikia. Ni raia wa mji ule muhimu. Tafadhali niruhusu niseme na watu.” Kamanda akamwambia Paulo unaweza kusema. Hivyo Paulo akasimama kwenye ngazi na kupunga mkono wake ili watu wanyamaze. Watu walinyamaza na Paulo akaanza kusema nao kwa Kiaramu. Paulo akasema, “Baba zangu na kaka zangu, nisikilizeni! Nitajitetea kwenu.” Wayahudi walipomsikia Paulo anazungumza kwa Kiaramu wakanyamaza. Kisha Paulo akasema, “Mimi ni Myahudi, nilizaliwa katika mji wa Tarso katika jimbo la Kilikia. Nilikulia hapa katika mji huu. Nilikuwa mwanafunzi wa Gamalieli ambaye kwa umakini alinifundisha kila kitu kuhusu sheria ya baba zetu. Daima nimekuwa na shauku ya kumheshimu Mungu, sawa na ninyi nyote hapa leo. Niliwatesa watu walioifuata Njia. Baadhi yao hapa waliuawa kwa sababu yangu. Niliwakamata wanaume na wanawake na kuwaweka gerezani. Kuhani mkuu na baraza lote la wazee wa Wayahudi wanaweza kuwathibitishia hili. Wakati mmoja viongozi hawa walinipa barua. Barua hizo waliandikiwa ndugu zetu Wayahudi katika mji wa Dameski. Nilikuwa naenda huko kuwakamata wafuasi wa Yesu na kuwaleta Yerusalemu ili waadhibiwe. Lakini kitu fulani kilinitokea nikiwa njiani kwenda Dameski. Ilipokuwa inakaribia mchana na nilikuwa karibu na mji wa Dameski. Ghafla mwanga kutoka mbinguni ulining'aria kunizunguka. Nilianguka chini na nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli kwa nini unanitesa?’ Niliuliza, ‘Wewe ni nani, Bwana?’ Sauti ikasema, ‘Mimi ni Yesu kutoka Nazareti, unayemtesa.’ Watu waliokuwa pamoja nami hawakuisikia sauti lakini waliona mwanga. Nilisema, ‘Nifanye nini Bwana?’ Bwana alinijibu, ‘Simama na uingie Dameski. Humo utawaambia yote niliyopanga uyafanye.’ Sikuweza kuona kwa sababu mwanga ule angavu ulinilemaza macho. Hivyo wale watu waliokuwa pamoja nami waliniongoza kuingia mjini Dameski. Alikuwepo mtu mmoja katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania. Mtu huyu alikuwa mcha Mungu na aliitii Sheria ya Musa na Wayahudi wote walioishi kule walimheshimu. Alikuja kwangu na kuniambia, ‘Sauli, ndugu yangu, tazama juu na uone tena!’ Ghafla niliweza kumwona. Anania aliniambia, ‘Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zetu alikuchagua wewe tangu zamani kuujua mpango wake. Amekuchagua wewe kumwona Mwenye Haki wake na kusikia maneno kutoka kwake. Utakuwa shahidi wake kwa watu wote. Utawaambia ulichoona na kusikia. Sasa usisubiri zaidi. Simama, ubatizwe na usafishwe dhambi zako, mwamini Yesu ili akuokoe.’ Baadaye, nilirudi Yerusalemu. Nilipokuwa naomba katika eneo la hekalu, nikaona maono. Nilimwona Yesu, naye akaniambia, ‘Haraka, ondoka Yerusalemu sasa hivi! Watu hapa hawataukubali ukweli unaowaambia kuhusu mimi.’ Nilisema, ‘Lakini, Bwana, Wayahudi wanajua kuwa mimi ndiye niliyewafunga gerezani na kuwapiga wale wanaokuamini wewe. Nilikwenda kwenye masinagogi yote kuwatafuta na kuwakamata Wayahudi wanaokuamini wewe. Watu wanajua pia kuwa nilikuwepo wakati Stefano shahidi wako, alipouawa. Nilisimama pale na kukubaliana nao kuwa wamwue. Nilishikilia hata mavazi ya watu waliokuwa wanamwua!’ Lakini Yesu akaniambia, ‘Ondoka sasa. Nitakutuma mbali sana kwa watu wasio Wayahudi.’” Watu waliacha kusikiliza Paulo aliposema jambo hili la mwisho. Walipasa sauti wote, wakisema, “Mwondosheni mtu huyu! Hastahili kuishi katika dunia hii tena.” Waliendelea kupiga kelele, wakichana nguo zao na kurusha mavumbi juu. Ndipo kamanda akawaambia askari wamwingize Paulo kwenye jengo la jeshi na wampige. Alitaka kumlazimisha Paulo aeleze ni kwa nini watu walikuwa wanampigia kelele namna ile. Askari walipokuwa wanamfunga Paulo, wakijiandaa kumpiga alimwuliza ofisa wa jeshi, “Je, mna haki ya kumpiga raia wa Rumi ambaye hajathibitika kuwa na hatia?” Ofisa aliposikia hili, alikwenda kwa kamanda na kumwambia. Ofisa alisema, “Unafahamu unalolifanya? Mtu huyu ni raia wa Rumi!” Kamanda akaenda kwa Paulo na kusema, “Niambie kwa hakika, ‘Je, wewe ni raia wa Rumi?’” Paulo akajibu, “Ndiyo.” Kamanda akasema, “Nililipa pesa nyingi kuwa raia wa Rumi.” Lakini Paulo akasema, “Nilizaliwa raia wa Rumi.” Ghafla watu waliokuwa wanajiandaa kumwuliza maswali Paulo waliondoka. Kamanda aliogopa kwa sababu alikuwa ameshamfunga Paulo kwa minyororo na ni raia wa Rumi. Siku iliyofuata kamanda alitaka kujua ni kwa nini Wayahudi wanamshitaki Paulo. Hivyo aliamuru viongozi wa makuhani na baraza kuu lote kukutana pamoja. Alimfungua Paulo minyororo na kumleta mbele ya baraza. Paulo aliwatazama wajumbe wa baraza na kusema, “Ndugu zangu, Nimeishi maisha yangu katika njia nzuri mbele za Mungu. Daima nimefanya yale niliyodhani ni haki.” Anania, kuhani mkuu alikuwa pale. Aliposikia hili, aliwaambia watu waliokuwa wamesisima karibu na Paulo wampige kwenye mdomo. Paulo akamwambia Anania, “Mungu atakupiga wewe pia! Wewe ni kama ukuta mchafu uliopakwa rangi nyeupe. Umeketi hapa na kunihukumu, ukitumia Sheria ya Musa. Lakini unawaambia wanipige wakati ni kinyume cha sheria.” Watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Una uhakika unataka kumtukana kuhani mkuu wa Mungu namna hiyo?” Paulo akasema, “Ndugu zangu, sikufahamu kuwa mtu huyu ni kuhani mkuu. Maandiko yanasema, ‘Usiseme mambo mabaya kuhusu kiongozi wa watu wako.’” Paulo alijua kuwa baadhi ya watu kwenye baraza lile ni Masadukayo na baadhi yao ni Mafarisayo. Hivyo akapaza sauti akasema, “Ndugu zangu, Mimi ni Farisayo na baba yangu ni Farisayo! Nimeshitakiwa hapa kwa sababu ninaamini kuwa watu watafufuka kutoka kwa wafu.” Paulo alipolisema hili, mabishano makubwa yakaanza kati ya Mafarisayo na Masadukayo. Baraza likagawanyika. (Masadukayo hawaamini katika ufufuo, malaika au roho. Lakini Mafarisayo wanaamini vyote.) Wayahudi hawa wote wakaanza kubishana kwa kupaza sauti. Baadhi ya walimu wa sheria, waliokuwa Mafarisayo wakasimama na kusema, “Hatuoni kosa lolote kwa mtu huyu. Inawezekana kwa hakika malaika au roho alizungumza naye.” Mabishano yaligeuka kuwa mapigano na kamanda aliogopa kwamba Wayahudi wangempasua Paulo vipande vipande. Hivyo akawaambia askari wateremke, wamwondoe Paulo na kumweka mbali na Wayahudi hao katika jengo la jeshi. Usiku uliofuata Bwana Yesu akaja na kusimama pembeni mwa Paulo. Akamwambia, “Uwe jasiri! Umewaambia watu kuhusu mimi humu Yerusalemu. Ni lazima ufanye vivyo hivyo Rumi.” Asubuhi iliyofuata baadhi ya Wayahudi walifanya mpango wa kumwua Paulo. Walijiapiza kuwa hawatakula wala kunywa kitu chochote mpaka watakapomwua Paulo. Walikuwa watu zaidi ya 40 waliofanya mpango huu. Walikwenda wakaongea na viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wa Wayahudi. Walisema, “Tumejiwekea nadhiri kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tumemwua Paulo. Tunataka mfanye hivi: Mtumieni kamanda ujumbe kutoka kwenu na baraza kuu. Mwambieni mnamtaka amlete Paulo kwenu. Semeni kwamba mnataka kumwuliza maswali zaidi, tutamwua akiwa njiani kuja hapa.” Lakini mpwaye Paulo aliusikia mpango huu. Alikwenda kwenye jengo la jeshi na kumwambia Paulo. Kisha Paulo akamwita mmoja wa maofisa wa jeshi na kumwambia, “Mchukue huyu kijana kwa kamanda. Ana ujumbe kwa ajili yake.” Hivyo ofisa wa jeshi akampeleka mpwaye Paulo kwa kamanda. Ofisa wa jeshi akasema, “Mfungwa Paulo ameniomba nimlete kijana huyu kwako. Ana kitu cha kukueleza.” Kamanda akamchukua kijana na kwenda naye mahali ambapo wangekuwa peke yao. Kamanda akamwuliza, “Unataka kuniambia nini?” Kijana akasema, “Baadhi ya Wayahudi wameamua kukuomba umpeleke Paulo kwenye mkutano wa baraza lao kesho. Wanataka wewe udhani kuwa wamepanga kumwuliza Paulo maswali zaidi. Lakini usiwaamini! Zaidi ya watu 40 miongoni mwao wamejificha na wanasubiri kumwua. Wote wameweka nadhiri kuwa hawatakula wala kunywa mpaka wamemwua Paulo. Sasa hivi wanasubiri wewe ukubali.” Kamanda akamtoa kijana, akamwambia, “Usimwambie yeyote kuwa umeniambia kuhusu mpango wao.” Ndipo Kamanda akawaita maofisa wawili wa jeshi. Akawaambia, “Ninataka baadhi ya watu kwenda Kaisaria. Andaeni askari mia mbili. Pia andaeni askari sabini waendao kwa farasi na mia mbili wa kubeba mikuki. Iweni tayari kuondoka saa tatu usiku. Andaeni baadhi ya farasi kwa ajili ya Paulo kuendesha ili aweze kupelekwa kwa Gavana Feliki salama.” Kamanda aliandika barua kuhusu Paulo. Hivi ndivyo alivyosema: Kutoka kwa Klaudio Lisiasi. Kwenda kwa Mheshimiwa Gavana Feliki. Salamu: Baadhi ya Wayahudi walimkamata mtu huyu na walikuwa karibu ya kumwua. Lakini nilipogundua kuwa ni raia wa Rumi, nilikwenda pamoja na askari wangu tukamwokoa. Nilitaka kufahamu kwa nini walikuwa wanamshitaki. Hivyo nikampeleka kwenye mkutano wa baraza lao. Hivi ndivyo nilivyoona: Wayahudi walisema mtu huyu alifanya mambo mabaya. Lakini mashitaka haya yalihusu sheria zao za Kiyahudi, na hakukuwa kosa lolote linaloweza kusababisha kufungwa au kifo. Nimeambiwa kuwa baadhi ya Wayahudi walikuwa wanafanya mpango wa kumwua. Hivyo nimeamua kumleta kwako. Pia nimewaambia Wayahudi hao wakwambie walichonacho dhidi yake. Askari walifanya kile walichoambiwa. Walimchukua Paulo na kumpeleka kwenye mji wa Antipatri usiku ule. Siku iliyofuata askari wa farasi walikwenda na Paulo mpaka Kaisaria, lakini askari wengine na wale wa mikuki walirudi kwenye jengo la jeshi mjini Yerusalemu. Askari wa farasi waliingia Kaisaria, wakampa barua Gavana Feliki, kisha wakamkabidhi Paulo kwake. Gavana akaisoma barua na kumwuliza Paulo, “Unatoka jimbo gani?” Gavana alitambua kuwa Paulo alikuwa anatoka Kilikia. Gavana akasema, “Nitakusikiliza Wayahudi wanaokushitaki watakapokuja hapa pia.” Kisha gavana akaamuru Paulo awekwe kwenye jumba la kifalme. (Jengo hili lilijengwa na Herode.) Siku tano baadaye Anania, kuhani mkuu, alikwenda mjini Kaisaria. Aliwachukua pamoja naye baadhi ya viongozi wa wazee wa Kiyahudi na mwanasheria aitwaye Tertulo. Walikwenda Kaisaria kutoa ushahidi dhidi ya Paulo mbele ya gavana. Paulo aliitwa kwenye mkutano, na Tertulo akaanza kueleza mashitaka. Tertulo alisema, “Mheshimiwa Feliki, kwa muda mrefu watu wetu wamefurahia amani kwa sababu yako, na mambo mengi mabaya katika nchi yetu yanarekebishwa kutokana na msaada wako wa hekima. Kwa hili sisi sote tunaendelea kushukuru. *** Lakini sitaki kuchukua muda wako mwingi. Hivyo nitasema maneno machache. Tafadhali uwe mvumilivu. Mtu huyu ni mkorofi. Anasababisha vurugu kwa Wayahudi kila mahali ulimwenguni. Ni kiongozi wa kundi la Wanazorayo. Pia, alikuwa anajaribu kulinajisi Hekalu, lakini tulimsimamisha. Unaweza kuamua ikiwa haya yote ni kweli. Mwulize maswali wewe mwenyewe.” *** *** Wayahudi wengine wakakubali na kusema ndivyo ilivyo. Gavana alifanya ishara ili Paulo aanze kuzungumza. Hivyo Paulo alijibu, “Gavana Feliki, ninafahamu kuwa umekuwa jaji wa nchi hii kwa muda mrefu. Hivyo ninafurahi kujitetea mimi mwenyewe mbele yako. Nilikwenda kuabudu Yerusalemu siku kumi na mbili tu zilizopita. Unaweza kutambua wewe mwenyewe kuwa hii ni kweli. Wayahudi hawa wanaonishitaki, hawakuniona nikibishana na mtu yeyote wala kukusanya kundi la watu Hekaluni. Na sikuwa nabishana au kufanya vurugu kwenye masinagogi au mahali popote katika mji. Watu hawa hawawezi kuthibitisha mambo wanayoyasema dhidi yangu sasa. Lakini nitakuambia hili: Ninamuabudu Mungu, Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zetu, na kama mfuasi wa Njia, ambayo wayahudi hawa wanasema si njia sahihi. Na ninaamini kila kitu kinachofundishwa katika Sheria ya Musa na yote yaliyoandikwa katika vitabu vya manabii. Nina tumaini katika Mungu kama walilonalo Wayahudi hawa, kwamba watu wote, wema na wabaya, watafufuliwa kutoka kwa wafu. Hii ndiyo sababu daima nimejaribu kufanya kile ninachoamini kuwa sahihi mbele za Mungu na kila mtu. Nimekuwa mbali na Yerusalemu kwa miaka mingi. Nilikwenda kule nikiwa na fedha za kuwasaidia watu wangu. Pia nilikuwa na sadaka za kutoa Hekaluni. Nilipokuwa nafanya hivyo, baadhi ya Wayahudi waliponiona pale. Nilikuwa nimemaliza ibada ya utakaso. Sikufanya vurugu yoyote, na hakuna watu waliokuwa wamekusanyika kunizunguka. *** Lakini baadhi ya Wayahudi kutoka Asia walikuwa pale. Walipaswa kuwa hapa mbele yako wakinishtaki ikiwa wana ushahidi kuwa nilifanya kitu chochote kibaya. Waulize watu hawa ikiwa waliona kosa lolote kwangu niliposimama mbele ya mkutano wa baraza kuu mjini Yerusalemu. Jibu pekee watakaloweza kukujibu ni hili: Kwamba nilipokuwa mbele zao nilipaza sauti na kusema, ‘Mnanishitaki leo kwa sababu ninaamini watu watafufuka kutoka kwa wafu!’” Feliki tayari alikuwa anaelewa mengi kuhusu Njia. Akasimamisha kesi na kusema, “Kamanda Lisiasi atakapokuja hapa, nitaamua nini cha kufanya.” Feliki alimwambia ofisa wa jeshi kumlinda Paulo lakini wampe uhuru kiasi na wawaruhusu rafiki zake wamletee chochote atakachohitaji. Baada ya siku chache, Feliki alikuja na mke wake Drusila, aliyekuwa Myahudi. Feliki akaagiza Paulo apelekwe kwake. Alimsikiliza Paulo akiongea kuhusu kumwamini Yesu Kristo. Lakini Feliki aliogopa Paulo alipoongelea kuhusu vitu kama kutenda haki, kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja baadaye. Akasema, “Unaweza kwenda sasa. Nitakapokuwa na muda mwingi, nitakuita.” Lakini Feliki alikuwa na sababu nyingine ya kuzungumza na Paulo. Alitegemea Paulo angempa rushwa, hivyo alimwita Paulo mara nyingi na kuzungumza naye. Lakini baada ya miaka miwili, Porkio Festo akawa gavana. Hivyo Feliki hakuwa gavana tena. Lakini alimwacha Paulo gerezani ili kuwaridhisha Wayahudi. Festo akawa gavana na siku tatu baadaye akasafiri kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria. Viongozi wa makuhani na viongozi maarufu wa Kiyahudi wakatoa mashitaka dhidi ya Paulo mbele ya Festo. Walimwomba Festo awasaidie. Walitaka amrudishe Paulo Yerusalemu kwa sababu walipanga kumwua akiwa njiani. Lakini Festo alijibu, “Hapana, Paulo ataendelea kuwekwa Kaisaria. Nitaenda huko mimi mwenyewe hivi karibuni, na viongozi wenu wanaweza kufuatana nami. Kama mtu huyu hakika amefanya chochote kibaya, wanaweza kumshitaki huko.” Festo alikaa Yerusalemu kwa siku nane au kumi zaidi kisha alirudi Kaisaria. Siku iliyofuata Festo akawaambia askari wamlete Paulo mbele yake. Festo alikuwa amekaa kwenye kiti cha hukumu. Paulo aliingia kwenye chumba na Wayahudi waliokuja kutoka Yerusalemu walisimama kumzunguka. Walileta mashitaka mengi mazito dhidi yake, lakini hawakuweza kuthibitisha chochote. Paulo alijitetea mwenyewe, akasema, “Sijatenda kitu chochote kibaya kinyume na sheria ya Kiyahudi, kinyume na Hekalu au kinyume na Kaisari.” Lakini Festo alitaka kuwaridhisha Wayahudi. Hivyo alimwuliza Paulo, “Unataka kwenda Yerusalemu ili nikakuhukumu huko kutokana na mashitaka haya?” Paulo akasema, “Kwa sasa nimesimama kwenye kiti cha hukumu cha Kaisari. Hapa ndipo ninatakiwa kuhukumiwa. Sijatenda lolote baya kwa Wayahudi na unafahamu hilo. Ikiwa nilitenda chochote kibaya na sheria inasema ni lazima nife, basi ninakubali kuwa ninapaswa kufa. Siombi kuokolewa kutokana na kifo. Lakini kama mashitaka haya siyo ya kweli, basi hakuna anayeweza kunikabidhi kwa watu hawa. Hapana, Nataka Kaisari aisikilize kesi yangu!” Festo alijadiliana na washauri wake kuhusu hili. Kisha akasema, “Umeomba kumwona Kaisari, basi utakwenda kwa Kaisari!” Siku chache baadaye Mfalme Agripa pamoja na dada yake aliyeitwa Bernike walikuja Kaisaria kumtembelea Festo. Walikaa huko kwa siku nyingi, na Festo akamwambia mfalme kuhusu kesi ya Paulo. Festo alisema, “Kuna mtu ambaye Feliki alimwacha gerezani. Nilipokwenda Yerusalemu, viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wa Kiyahudi walitengeneza mashitaka dhidi yake. Walinitaka nimhukumu kifo. Lakini niliwaambia, ‘Mtu anaposhitakiwa kuwa ametenda jambo baya, Warumi hawampeleki kwa watu wengine ili ahukumiwe. Kwanza, ni lazima aonane na watu wanaomshtaki. Na kisha ni lazima aruhusiwe kujitetea yeye mwenyewe dhidi ya mashitaka yao.’ Hivyo Wayahudi walipokuja hapa kwa ajili ya kesi, sikupoteza muda. Siku iliyofuata nilikaa kwenye kiti cha hukumu na kuamuru Paulo aletwe ndani. Wayahudi walisimama na kumshitaki. Lakini hawakumshitaki kwa makosa niliyodhani wangemshitaki. Mashitaka yao yote yalihusu dini yao wenyewe na kuhusu mtu anayeitwa Yesu. Yesu alikufa lakini Paulo anasema bado yuko hai. Baada ya kuona kuwa sijui jinsi ya kuyachunguza mambo haya. Hivyo nilimwuliza Paulo, ‘Unataka kwenda Yerusalemu ili ukahukumiwe huko?’ Lakini Paulo aliomba abaki mahabusu hapa Kaisaria. Anataka uamuzi kutoka kwa mfalme mkuu. Hivyo niliamua aendelee kushikiliwa hapa mpaka nitakapompeleka kwa Kaisari huko Rumi.” Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyu pia.” Festo akasema, “Utaweza kumsikiliza kesho.” Siku iliyofuata Agripa na Bernike walikuja kwenye mkutano kwa fahari kubwa, wakijifanya watu wa muhimu sana. Waliingia kwenye chumba pamoja na viongozi wa kijeshi na watu maarufu wa mji. Festo akawaamuru askari wamwingize Paulo ndani. Festo akasema, “Mfalme Agripa nanyi nyote mliokusanyika hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu. Wayahudi wote, hapa na Yerusalemu wamelalamika kwangu juu yake. Wanapolalamika, wanapaza sauti zao wakisema kwamba anapaswa kuuawa. Nilipochunguza, sikuona ikiwa alitenda kosa lolote linalostahili hukumu ya kifo. Lakini ameomba kuhukumiwa na Kaisari, hivyo niliamua apelekwe Rumi. Hata hivyo, sifahamu kwa hakika ni nini cha kumwandikia bwana wangu Kaisari kama sababu ya kumpeleka mtu huyu kwake. Hivo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa wewe, Mfalme Agripa. Ninatumaini kwamba utamwuliza maswali na kunipa kitu cha kumwandikia Kaisari. Nafikiri ni upumbavu kupeleka mfungwa kwa Kaisari bila kuainisha mashitaka dhidi yake.” Agripa akamwambia Paulo, “Unaweza sasa kujitetea wewe mwenyewe.” Paulo akanyoosha mkono wake ili wamsikilize kwa makini na akaanza kusema. “Mfalme Agripa, najisikia heshima kusimama hapa mbele yako leo ili nijibu mashitaka yote yaliyotengenezwa na Wayahudi dhidi yangu. Ninafurahi kuzungumza nawe, kwa sababu unafahamu sana kuhusu desturi za Kiyahudi na mambo ambayo Wayahudi hubishana. Tafadhali uwe mvumilifu kunisikiliza. Wayahudi wote wanafahamu maisha yangu yote. Wanafahamu namna nilivyoishi tangu mwanzo miongoni mwa watu mwangu na baadaye Yerusalemu. Wayahudi hawa wamenifahamu kwa muda mrefu. Wakitaka wanaweza kukwambia kwamba nilikuwa Farisayo mzuri. Na Mafarisayo wanazitii sheria za dini ya Kiyahudi kwa uangalifu kuliko kundi lolote. Na sasa nimeshitakiwa kwa sababu ninatumaini ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu. Hii ni ahadi ambayo makabila yote kumi na mbili ya watu wetu yanatumaini kuipokea. Kwa sababu ya tumaini hili Wayahudi wanamtumikia Mungu usiku na mchana. Ee Mfalme wangu, Wayahudi wamenishitaki kwa sababu ninatumaini ahadi hii hii. Kwa nini ninyi watu mnadhani Mungu hawezi kuwafufua watu kutoka kwa wafu? Huko nyuma nilidhani kuwa ninapaswa kufanya kinyume na Yesu kutoka Nazareti kwa kadri ninavyoweza. Na ndivyo nilivyofanya, kuanzia Yerusalemu. Viongozi wa makuhani walinipa mamlaka ya kuwaweka gerezani watu wa Mungu wengi. Na walipokuwa wanauawa nilikubali kuwa lilikuwa jambo zuri. Nilikwenda katika masinagogi yote na kuwaadhibu, nikijaribu kuwafanya wamlaani Yesu. Hasira yangu dhidi ya watu hawa ilikuwa kali sana kiasi kwamba nilikwenda katika miji mingine kuwatafuta na kuwaadhibu. Wakati fulani viongozi wa makuhani walinipa ruhusa na mamlaka kwenda katika mji wa Dameski. Nikiwa njiani, mchana, niliona mwanga kutoka mbinguni, unaong'aa kuliko jua. Uling'aa kunizunguka mimi pamoja na wale waliokuwa wanasafiri pamoja nami. Sote tulianguka chini. Kisha nilisikia sauti iliyozungumza nami kwa Kiaramu. Sauti ilisema, ‘Sauli, Sauli, kwa nini unanitesa? Unajiumiza wewe mwenyewe kwa kunipinga mimi.’ Nilisema, ‘Wewe ni nani, Bwana?’ Bwana alisema, ‘Mimi ni Yesu. Unayemtesa. Simama! Nimekuchagua wewe kuwa mtumishi wangu. Utawaambia watu habari zangu, ulichoona leo na yale nitakayokuonesha. Hii ndiyo sababu nimekuja kwako. Nitakulinda dhidi ya watu wako na dhidi ya watu wasio Wayahudi, ninaokutuma kwao. Utawafanya waielewe kweli. Watatoka gizani na kuja kwenye mwanga. Watageuka kutoka kwenye mamlaka ya Shetani na kumgeukia Mungu. Ndipo dhambi zao zitasamehewa, na wataweza kupewa nafasi miongoni mwa watu wa Mungu, walifanywa watakatifu kwa kuniamini.’” Paulo aliendelea kusema: “Mfalme Agripa, baada ya kuona maono haya kutoka mbinguni, nilitii. Nilianza kuwaambia watu kubadili mioyo na maisha yao na kumgeukia Mungu. Niliwaambia kufanya yale yatakayoonyesha kwamba hakika wamebadilika. Kwanza nilikwenda kwa watu waliokuwa Dameski. Kisha nikaenda Yerusalemu na kila sehemu ya Uyahudi na nikawaambia watu huko. Nilikwenda pia kwa watu wasio Wayahudi. Hii ndiyo sababu Wayahudi walinikamata na kujaribu kuniua Hekaluni. Lakini Mungu alinisaidia, na bado ananisaidia leo. Kwa msaada wa Mungu nimesimama hapa leo na kuwaambia watu kile nilichokiona. Lakini sisemi chochote kipya. Ninasema kile ambacho Musa na manabii walisema kingetokea. Walisema kwamba Masihi atakufa na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu. Walisema kwamba ataleta mwanga wa kweli ya Mungu inayowaokoa wote, Wayahudi na wasio Wayahudi.” Paulo alipokuwa bado anajitetea, Festo alipaza sauti akasema, “Paulo, umerukwa na akili! Kusoma kwingi kumekufanya kichaa.” Paulo akasema, “Mheshimiwa Festo, mimi si kichaa. Ninachokisema ni kweli na kinaingia akilini. Mfalme Agripa analifahamu hili, na ninaweza kuzungumza naye kwa uhuru. Ninafahamu kwamba amekwisha kusikia kuhusu mambo haya, yalitokea mahali ambako kila mtu aliyaona. Mfalme Agripa, unaamini yale ambayo manabii waliandika? Ninajua unaamini!” Mfalme Agripa akamwambia Paulo, “Unadhani unaweza kunishawishi kirahisi kiasi hicho ili niwe Mkristo?” Paulo akasema, “Haijalishi kwangu, ikiwa ni vigumu au rahisi. Ninaomba tu kwa Mungu kwamba si wewe peke yako lakini kila mtu anayenisikiliza leo angeokolewa ili awe kama mimi, isipokuwa kwa minyororo hii!” Mfalme Agripa, Gavana Festo, Bernike, na watu wote waliokaa pamoja nao wakasimama na kuondoka chumbani. Walikuwa wanaongea wenyewe. Walisema, “Mtu huyu hajafanya chochote kinachostahili kuuawa au kuwekwa gerezani.” Kisha Agripa akamwambia Festo, “Tungemwachia huru, lakini ameomba kumwona Kaisari.” Iliamriwa kwamba tutakwenda Italia. Ofisa wa Jeshi aliyeitwa Yulio, aliyetumika katika jeshi maalumu la mfalme mkuu, aliwekwa kuwa kiongozi wa kumlinda Paulo na baadhi ya wafungwa wengine safarini. Tuliingia kwenye meli katika mji wa Adramatio. Meli hiyo ilikuwa inasafiri kupitia sehemu mbalimbali za Asia. Aristarko, mtu Thesalonike katika makedonia alisafiri pamoja nasi. Siku iliyofuata tulifika kwenye mji wa Sidoni. Yulio alikuwa mwema sana kwa Paulo na akampa uhuru wa kwenda kuwatembelea rafiki zake pale, walimpa chochote alichohitaji. Tuliondoka katika mji ule na tukatweka tanga tukasafiri karibu na kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa unavuma kinyume nasi. Tulikwenda kwa kukatisha bahari upande wa Kilikia na Pamfilia. Kisha tukafika katika mji wa Mira katika jimbo la Likia. Tulipofika hapo ofisa wa jeshi akapata meli iliyotoka katika mji wa Iskanderia iliyokuwa inakwenda Italia. Akatupandisha humo. Tulitweka tanga na kusafiri taratibu kwa siku nyingi. Ilikuwa vigumu kwetu kufika katika mji wa Nido kwa sababu upepo ulikuwa unavuma kinyume chetu. Hatukuweza kuendelea zaidi kwa kupitia njia hiyo, hivyo tulitweka tanga tukasafiri kupitia upande wa kusini mwa kisiwa cha Krete karibu na Salmone. Tulisafiri sambamba na pwani, lakini kwa shida. Ndipo tukafika mahali palipoitwa Bandari Salama, karibu na mji wa Lasea. Tulikuwa tumepoteza muda mwingi, na ilikuwa hatari kutweka tanga, kwa sababu tayari ilikuwa baada ya siku ya Kiyahudi ya kufunga. Hivyo Paulo aliwaonya akasema, “Ndugu zangu, ninaona kuwa kutakuwa shida nyingi katika safari hii. Meli, kila kitu ndani yake na pia hata maisha yetu yanaweza kupotea!” Lakini nahodha na mmiliki wa meli hawakukubaliana na Paulo. Hivyo ofisa wa jeshi alikubali walichokisema badala ya kumwamini Paulo. Pia, bandari ile haikuwa mahali pazuri kwa meli kukaa majira ya baridi, hivyo watu karibu wote wakaamua kwamba ni lazima tuondoke pale. Walitegemea kuwa tungeweza kufika Foeniki, ambako meli ingekaa majira ya baridi. Foeniki ulikuwa mji katika kisiwa cha Krete. Ulikuwa na bandari iliyotazama Kusini-Magharibi na Kaskazini-Magharibi. Ndipo upepo mzuri ukaanza kuvuma kutoka kusini. Watu ndani ya meli wakafikiri, “Huu ndio upepo tulioutaka, na sasa tumeupata!” Hivyo wakavuta nanga. Tulitweka tanga tukasafiri karibu na kisiwa cha Krete. Lakini upepo wenye nguvu unaoitwa “Kaskazini-Mashariki” ulikuja kwa kukikatisha kisiwa. Upepo huu uliichukua meli na kuisukumia mbali. Meli haikuweza kwenda kinyume na upepo, hivyo tulisimama tukijaribu kuuacha upepo utusukume. Tulikwenda upande wa chini wa kisiwa kidogo kilichoitwa Kauda. Kisiwa kikatukinga dhidi ya upepo, tulichukua mtumbwi wa kuokolea watu, lakini ilikuwa vigumu sana kufanya hivyo. Baada ya watu kuleta mtumbwi wa kuokolea, wakaifunga meli kamba kuizungushia ili iendelee kushikamana isipasuke. Waliogopa kwamba meli ingekwama kwenye mchanga wa pwani ya Sirti. Hivyo walishusha tanga na kuiacha meli ichukuliwe na upepo. Siku iliyofuata upepo ulivuma kinyume nasi kwa nguvu kiasi kwamba watu walitupa baadhi ya vitu kutoka katika shehena ya meli. Siku moja baadaye wakatupa vifaa vya meli. Kwa siku nyingi hatukuweza kuliona jua au nyota. Dhoruba ilikuwa mbaya sana. Tulipoteza matumaini yote ya kuendelea kuwa hai, tulidhani tutakufa. Watu hawakula kwa muda mrefu. Ndipo siku moja Paulo akasimama mbele yao na kusema, “Ndugu zangu, niliwaambia tusiondoke Krete. Mngenisikiliza msingepata tatizo hili na hasara hii. Lakini sasa ninawaambia iweni na furaha. Hakuna hata mmoja wenu atakayekufa, lakini meli itapotea. Usiku uliopita malaika kutoka kwa Mungu ninayemwabudu na ambaye mimi ni wake. Aliniambia, ‘Paulo, usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari. Mungu amekupa ahadi hii: Ataokoa maisha ya wote wanaosafiri pamoja nawe.’ Hivyo ndugu, msihofu kitu chochote. Ninamwamini Mungu, na nina uhakika kila kitu kitatokea kama malaika wake alivyoniambia. Lakini tutajigonga kwenye kisiwa.” Usiku wa kumi na nne tulikuwa bado tunasukumwa na upepo katika bahari ya Adriatiki. Mabaharia wakadhani tulikuwa karibu na nchi kavu. Wakatupa kamba iliyofungwa kitu kizito kwenye ncha yake. Wakakuta kwamba kina cha maji ni futi mia moja na ishirini. Wakaendelea mbele kidogo na kutupa kamba tena. Kina kilikuwa futi tisini. Mabaharia waliogopa kwa kudhani kwamba tungegonga miamba, hivyo wakatupa nanga nne kwenye maji. Kisha wakaomba mchana ufike. Baadhi ya mabaharia walitaka kuiacha meli, waliishusha majini mtumbwi wa kuokolea. Walitaka watu wengine wadhani kuwa walikuwa wanatupa nanga upande wa mbele wa meli. Lakini Paulo alimwambia ofisa wa jeshi na askari wengine, “Iwapo watu hawa hawatakaa ndani ya meli, mtapoteza matumaini yote ya kupona.” Hivyo askari wakakata kamba na kuuacha mtumbwi uanguke majini. Kabla ya kupambazuka Paulo alianza kuwashawishi watu wote kula. Alisema, “Kwa wiki mbili mmekuwa mnasubiri na kuangalia, hamjala kwa siku kumi na nne. Sasa ninawasihi mle chakula, mnakihitaji ili kuishi. Hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza hata unywele mmoja kutoka kwenye kichwa chake.” Baada ya kusema hili, Paulo alichukua baadhi ya mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya mikate hiyo mbele yao wote. Akakata kipande na kuanza kula. Watu wote wakafarijika na kuanza kula pia. (Walikuwemo watu mia mbili sabini na sita ndani ya meli.) Tulikula kila tulichohitaji. Kisha tukaanza kumwaga nafaka baharini ili meli iwe nyepesi. Mchana ulipofika, mabaharia waliiona nchi kavu, lakini hawakupafahamu mahali pale. Waliona ghuba yenye ufukwe na walitaka kuipeleka meli ufukweni ikiwa wangeweza. Hivyo walikata kamba kwenye nanga na kuziacha nanga ndani ya bahari. Wakati huo huo walifungua kamba zilizokuwa zinaushikilia usukani. Kisha wakanyanyua tanga la mbele na kutweka tanga kuelekea ufukweni. Lakini meli uligonga mwamba wa michanga. Sehemu ya mbele ya meli ilikwama pale na haikuweza kutoka. Kisha mawimbi makubwa yakaanza kuvunja sehemu ya nyuma ya meli vipande vipande. Askari waliamua kuwaua wafungwa ili asiwepo mfungwa hata mmoja atakayeogelea na kutoroka. Lakini Yulio, ofisa wa jeshi alitaka Paulo asiuawe. Hivyo hakuwaruhusu askari kuwaua wafunga. Aliwaambia watu wanaoweza kuogelea, waruke majini kwenda nchi kavu. Wengine walitumia mbao au vipande vya meli. Hivi ndivyo ambavyo watu wote walifika nchi kavu wakiwa salama. Tulipokuwa salama nchi kavu, tukatambua kuwa kisiwa kile kinaitwa Malta. Watu walioishi pale walikuwa wema sana kwetu. Mvua ilikuwa inanyesha na kulikuwa baridi sana, hivyo walitengeneza moto na kutukaribisha sote. Paulo alikusanya kuni nyingi kwa ajili ya moto. Alipokuwa akiweka kuni kwenye moto, nyoka mwenye sumu kali akajitokeza kwa sababu ya joto na kumuuma kwenye mkono. Wenyeji wa kisiwa kile walipomwona nyoka ananing'inia kwenye mkono wa Paulo, walisema, “Mtu huyu lazima ni mwuaji! Hakufa baharini, lakini Haki hataki aishi.” Lakini Paulo alimku'ngutia nyoka kwenye moto na hakudhurika. Watu wakadhani atavimba au ataanguka na kufa. Walisubiri na kumwangalia kwa muda mrefu, lakini hakuna kibaya kilichomtokea. Hivyo wakabadili mawazo yao. Wakasema, “Paulo ni mungu!” Yalikuwepo mashamba kuzunguka eneo lile. Yaliyomilikiwa na ofisa wa juu sana wa Rumi katika kisiwa hicho aliyeitwa Pablio. Alitukaribisha nyumbani kwake na alikuwa mwema sana kwetu. Tulikaa nyumbani kwake kwa siku tatu. Baba yake Pablio alikuwa mgonjwa sana. Alikuwa na homa na alikuwa anaharisha damu, lakini Paulo alikwenda kwake na kumuombea. Aliweka mikono juu yake naye akapona. Baada ya hili kutokea, wagonjwa wengine wote kisiwani walikuja kwa Paulo, naye aliwaombea na wakaponywa pia. Watu katika kisiwa hiki walituheshimu sana. Na baada ya kuwa pale kwa miezi mitatu, tukawa tayari kuondoka, walitupa kila kitu tulichohitaji kwa ajili ya safari yetu. Tulipanda meli iliyotoka Iskanderia iliyokaa katika kisiwa cha Malta wakati majira ya baridi. Mbele ya meli kulikuwa alama ya miungu pacha. *** Tulisimama katika mji wa Sirakuse. Tulikaa pale kwa siku tatu kisha tukaondoka. Tulifika katika mji wa Regio. Siku iliyofuata upepo ulianza kuvuma kutokea Kusini-Magharibi, hivyo tuliweza kuondoka. Baada ya siku moja tukafika katika mji wa Puteoli. Tuliwapata baadhi ya waamini pale, walituomba tukae nao kwa wiki moja. Mwishowe tulifika Rumi. Ndugu na dada waliokaa Rumi walisikia habari zetu, walikuja kutupokea kwenye Soko la Apio na kwenye Migahawa Mitatu. Paulo alipowaona waamini hawa, alimshukuru Mungu na alifarijika. Tulipofika Rumi, Paulo aliruhisiwa kuishi peke yake. Lakini askari alikaa pamoja naye kumlinda. Siku tatu baadaye Paulo aliagiza baadhi ya Wayahudi muhimu waje kwake. Walipokusanyika, akasema, “Ndugu zangu, sijafanya lolote kinyume na watu wetu au kinyume na desturi za baba zetu. Lakini nilikamatwa Yerusalemu na kukabidhiwa kwa Warumi. Waliniuliza maswali mengi, lakini hawakupata sababu yoyote kwa nini niuawe. Hivyo walitaka kuniachia huru. Lakini Wayahudi kule hawakutaka hilo. Hivyo ilinibidi niombe kuja Rumi kuweka mashitaka yangu mbele ya Kaisari. Kwa kufanya hivi haimaanishi kuwa ninawashutumu watu wangu kwa kufanya chochote kibaya. Ndiyo sababu nilitaka kuonana na kuzungumza nanyi. Nimefungwa kwa minyororo hii kwa sababu ninaamini katika tumaini la Israeli.” Wayahudi walimjibu Paulo, “Hakuna barua tuliyoipokea kutoka Uyahudi kuhusu wewe. Hakuna ndugu yetu yeyote Myahudi aliyesafiri kutoka huko aliyeleta habari zako au kutwambia chochote kibaya juu yako. Tunataka kusikia mawazo yako. Tunafahamu kuwa watu kila mahali wanapinga kundi hili jipya.” Paulo na Wayahudi walichagua siku kwa ajili ya mkutano. Siku hiyo Wayahudi wengi walikutana na Paulo katika nyumba yake. Aliwaambia kwa siku nzima, akawafafanulia kuhusu ufalme wa Mungu. Alitumia Sheria ya Musa na maandishi ya manabii kuwashawishi kumwamini Yesu. Baadhi ya Wayahudi waliamini alichosema, lakini wengine hawakuamini. Walibishana wao wenyewe na wakaanza kuondoka. Lakini aliwaambia kitu kimoja zaidi: “Roho Mtakatifu aliwaambia ukweli baba zenu kupitia nabii Isaya, aliposema, ‘Nenda kwa watu hawa na uwaambie: Mtasikiliza na kusikiliza, lakini hamtaelewa. Mtatazama na kutazama, lakini hakika hamtaona. Watu hawa hawawezi kuelewa. Masikio yao yamezibwa. Na macho yao yamefumbwa. Hivyo hawawezi kuona kwa macho yao, au kusikia kwa masikio yao; au kuelewa kwa akili zao; au kuelewa kwa akili zao. Ikiwa wangeelewa, wangeweza kunirudia, na ningewaponya.’ Ninataka ninyi Wayahudi mjue kuwa Mungu ameupeleka wokovu wake kwa watu wasio Wayahudi. Watasikia!” *** Paulo alikaa katika nyumba yake mwenyewe aliyopanga kwa miaka miwili kamili. Aliwakaribisha watu wote waliokuja kumtembelea. Aliwaambia kuhusu ufalme wa Mungu na kuwafundisha kuhusu Bwana Yesu Kristo. Alikuwa na ujasiri sana, na hakuna aliyejaribu kumzuia asizungumze. Salamu kutoka kwa Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu. Mungu alinichagua niwe mtume na akanipa kazi ya kuhubiri Habari Njema yake. Tangu zamani, kwa vinywa vya manabii katika Maandiko Matakatifu, Mungu aliahidi kwamba angewaletea Habari Njema watu wake. Habari Njema hii inahusu Mwana wa Mungu, ambaye kama mwanadamu, alizaliwa katika ukoo wa Mfalme Daudi. Na alipofufuliwa na Roho Matakatifu kutoka kwa wafu, alipewa mamlaka kamili ya kutawala kama Mwana wa Mungu. Ni Yesu Kristo, Bwana wetu. Kupitia kwa Yesu, Mungu amenionyesha wema wake. Na amenipa mamlaka ya kuwaendea watu wa mataifa yote na kuwaongoza kumwamini na kumtii yeye. Kazi yote hii ni kwa ajili yake. Nanyi pia ni miongoni mwa waliochaguliwa na Mungu ili mmilikiwe na Yesu Kristo. Waraka huu ni kwa ajili yenu ninyi nyote mlio huko Rumi. Kwani Mungu anawapenda na amewachagua kuwa watu wake watakatifu. Ninamwomba Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo, wawape ninyi neema na amani. Kwanza, ninamshukuru Mungu wangu kupitia Yesu Kristo kwa ajili yenu ninyi nyote. Ninamshukuru yeye kwa sababu kila mahali ulimwenguni watu wanazungumza kuhusu imani yenu kuu. Kila wakati ninapoomba, ninawakumbuka ninyi daima. Mungu anajua kuwa hii ni kweli. Yeye ndiye ninayemtumikia kwa moyo wangu wote nikiwaambia watu Habari Njema kuhusu Mwanaye. Hivyo ninaendelea kuomba kwamba mwishowe Mungu atanifungulia njia ili niweze kuja kwenu. *** Ninataka sana niwaone na niwape zawadi ya kiroho ili kuimarisha imani yenu. Ninamaanisha kuwa ninataka tusaidiane sisi kwa sisi katika imani tuliyo nayo. Imani yenu itanisaidia mimi, na imani yangu itawasaidia ninyi. Kaka zangu na dada zangu, ninataka mjue kwamba nimepanga mara nyingi kuja kwenu, lakini jambo fulani hutokea na kubadili mipango yangu kila ninapopanga kuja. Juu ya kazi yangu miongoni mwenu, ningependa kuona matokeo yale yale mazuri yakitokea ya kazi yangu miongoni mwa watu wengine wasio Wayahudi. Imenilazimu kuwatumikia watu wote; waliostaarabika na wasiostaarabika, walioelimika na wasio na elimu. Ndiyo sababu ninataka sana kuzihubiri Habari Njema kwenu ninyi pia mlio huko Rumi. Kwa mimi hakuna haya katika kuhubiri Habari Njema. Ninayo furaha kwa sababu Habari Njema ni nguvu ya Mungu inayomwokoa kila anayeamini, yaani inawaokoa Wayahudi kwanza, na sasa inawaokoa Mataifa. Ndiyo, wema wa uaminifu wa Mungu umedhihirishwa katika Habari Njema kwa uaminifu wa mmoja, ambao huongoza imani ya wengi. Kama Maandiko yanavyosema, “Aliye na haki mbele za Mungu ataishi kwa imani.” Mungu huonesha hasira yake kutokea mbinguni dhidi ya mambo mabaya ambayo waovu hutenda. Hawamheshimu na wanatendeana mabaya. Maisha yao maovu yanasababisha ukweli kuhusu Mungu usijulikane. Hili humkasirisha Mungu kwa sababu wamekwisha oneshwa Mungu alivyo. Ndiyo, Mungu ameliweka wazi kwao. Yapo mambo yanayoonekana kuhusu Mungu, kama vile nguvu zake za milele na yale yote yanayomfanya awe Mungu. Lakini tangu kuumbwa kwa ulimwengu, mambo haya yamekuwa rahisi kwa watu kuyaona. Maana yake ni kuwa, watu wanaweza kumwelewa Mungu kwa kuangalia yale aliyoumba. Hivyo watu hawana udhuru kwa uovu wanaotenda. Watu walimjua Mungu, lakini hawakumheshimu kama Mungu. Na hawakumpa shukrani. Badala yake waliyageukia mambo ya hovyo yasiyo na manufaa. Akili zao zilichochanganyikiwa zilijaa giza. Walisema kuwa wana hekima, lakini wakawa wajinga. Hawakuuheshimu ukuu wa Mungu, anayeishi milele. Wakaacha kumwabudu Mungu wakaanza kuabudu sanamu, vitu vilivyotengenezwa vikaonekana kama wanadamu, ambao wote mwisho hufa, au kwa mfano wa ndege na wanyama wanaotembea na wanaotambaa. Hivyo Mungu akawaacha wazifuate tamaa zao chafu. Wakawa najisi na wakaivunjia heshima miili yao kwa njia za uovu walizotumia. Waliibadili kweli kuhusu Mungu kwa uongo. Wakasujudu na kuabudu vitu alivyoviumba Mungu badala ya kumwabudu Mungu aliyeviumba vitu hivyo. Yeye ndiye anayepaswa kusifiwa milele yote. Amina. Hivyo, kwa kuwa watu hawakumheshimu Mungu, Mungu akawaacha wafuate tamaa zao za aibu. Wanawake wao wakabadili namna ya kujamiiana na wakawatamani wanawake wenzao na wakajamiiana wao kwa wao. Wanaume wakafanya vivyo hivyo. Wakaacha kujamiiana na wanawake kwa mfumo wa asili, wakaanza kuwawakia tamaa wanaume wenzao. Wakafanya mambo ya aibu na wanaume na wavulana. Wakajiletea aibu hii juu yao wenyewe, wakapata yale waliyostahili kwa kutelekeza kweli. Watu hawa waliona kuwa haikuwa muhimu kwao kumkubali Mungu katika fikra zao. Hivyo Mungu akawaacha wayafuate mawazo yao mabaya. Hivyo hufanya mambo ambayo mtu yeyote hapaswi kufanya. Maisha yao yamejaa kila aina ya matendo mabaya, uovu, tamaa na chuki. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, uongo na hamu ya kuwadhuru wengine. Wanasengenya na kusemana maovu wao wenyewe. Wanamchukia Mungu. Ni wakorofi, wana kiburi na hujivuna. Hubuni njia za kufanya maovu. Hawawatii wazazi wao. Ni wapumbavu, hawatimizi ahadi zao. Hawawaoneshi wema wala huruma wengine. Wanajua amri ya Mungu kuwa yeyote anayeishi kwa namna hiyo lazima afe. Lakini si tu kwamba wanaendelea kufanya mambo haya wenyewe, bali wanakubaliana na wengine wanaofanya mambo hayo. Je, unadhani unaweza kuwahukumu watu wengine? Unakosea. Wewe pia una hatia ya dhambi. Unawahukumu kwa kuwa wanatenda mabaya, lakini wewe unatenda yale wanayotenda. Hivyo unapowahukumu, unajihukumu wewe mwenyewe. Lakini tunajua kwamba Mungu yuko sahihi kwa kuwahukumu wote wanaotenda mambo ya jinsi hiyo! Lakini kwa kuwa unatenda mambo sawa na wale unaowahukumu, hakika unaelewa kuwa Mungu atakuadhibu nawe pia. Unawezaje kufikiri kuwa utaiepuka hukumu yake? Mungu amekuwa mwema kwako. Na amekuwa mvumilivu sana, akisubiri ubadilike. Lakini haufikirii jambo lolote kuhusu wema wake mkuu. Pengine huelewi kwamba Mungu ni mwema kwako ili ubadili moyo na maisha yako. Lakini wewe ni mkaidi sana! Unakataa kubadilika. Hivyo unaikuza hukumu yako wewe mwenyewe zaidi na zaidi. Utahukumiwa siku ile ambapo Mungu ataonesha hasira yake. Siku ambayo kila mtu ataona Mungu anavyowahukumu watu kwa haki. Kama anavyosema, “Atamlipa au kumwadhibu kila mtu kutokana na matendo yale.” Watu wengine hawachoki kutenda mema. Wanaishi kwa ajili ya utukufu na heshima kutoka kwa Mungu na kwa ajili ya maisha yasiyoweza kuharibiwa. Mungu atawapa watu hao uzima wa milele. Lakini wengine hutenda mambo yanayowafurahisha wao wenyewe. Hivyo hukataa yaliyo haki na huchagua kutenda mabaya. Watateseka kwa hukumu ya Mungu yenye hasira. Matatizo na mateso yatampata kila mmoja anayetenda uovu; kuanzia Wayahudi kwanza kisha wale wasio Wayahudi. Lakini atampa utukufu, heshima na amani kila atendaye mema; wale wote wanaotenda mema; kuanzia Wayahudi kwanza kisha wale wasio Wayahudi. Ndiyo, Mungu humhukumu kila mtu pasipo upendeleo, bila kujali yeye ni nani. Watu walio na sheria na wote ambao hawajawahi kuisikia sheria, wote wako sawa wanapotenda dhambi. Watu wasio na sheria na ni watenda dhambi wataangamizwa. Vivyo hivyo, wale walio na sheria na ni watenda dhambi watahukumiwa kuwa na hatia kwa kutumia sheria. Kuisikia sheria hakuwafanyi watu wawe wenye haki kwa Mungu. Wanakuwa wenye haki mbele zake, pale wanapotekeleza kile kinachoagizwa na sheria. Fikirini kuhusu wasio Wahayudi ambao hawakukua wakiwa na sheria. Wanapotenda kama sheria inavyoamuru, wanakuwa kielelezo cha sheria, ijapokuwa hawana sheria iliyoandikwa. Wanaonesha kuwa wanafahamu kilicho sahihi na kibaya, kama sheria inavyoamuru na dhamiri zao zinakubali. Lakini wakati mwingine mawazo yao huwaambia kuwa wamekosea au wamefanya sahihi. Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ambayo Mungu atazihukumu siri za watu kupitia Yesu Kristo, sawasawa na Habari Njema ninayoihubiri. Wewe unajiita Myahudi, na unajiona upo salama kwa kuwa tu una sheria. Kwa majivuno unadai kuwa wewe ni mmoja wa wateule wa Mungu. Unajua yale ambayo Mungu anataka ufanye. Na unajua yaliyo muhimu, kwa sababu umejifunza sheria. Unadhani kuwa wewe ni kiongozi wa watu wasioweza kuiona njia sahihi, na nuru kwa wale walio gizani. Unafikiri unaweza kuwaonesha wajinga kilicho sahihi. Na unadhani kuwa wewe ni mwalimu wa wanaoanza kujifunza. Unayo sheria, na hivyo unadhani unajua kila kitu na una kweli yote. Unawafundisha wengine, sasa kwa nini usijifundishe wewe wenyewe? Unawaambia usiibe, lakini wewe mwenyewe unaiba. Unasema wasizini, lakini wewe mwenyewe una hatia ya dhambi hiyo. Unachukia sanamu, lakini unaziiba sanamu katika mahekalu yao. Unajivuna sana kwamba una sheria ya Mungu, lakini unamletea Mungu aibu kwa kuivunja sheria yake. Kama Maandiko yanavyosema, “Watu wa mataifa mengine wanamtukana Mungu kwa sababu yako.” Ikiwa mnaifuata sheria, basi kutahiriwa kwenu kuna maana. Lakini mkiivunja sheria, mnakuwa kama watu ambao hawakutahiriwa. Wale wasiokuwa Wayahudi hawatahiriwi. Lakini wakiifuata sheria inavyosema, wanakuwa kama watu waliotahiriwa. Mnayo sheria na tohara, lakini mnaivunja sheria. Hivyo wale wasiotahiriwa katika miili yao, lakini bado wanaitii sheria, wataonesha kuwa mna hatia. Wewe si Myahudi halisi ikiwa utakuwa Myahudi tu kwa nje. Tohara halisi si ile ya nje ya mwili tu. Myahudi halisi ni yule aliye Myahudi kwa ndani. Tohara halisi inafanywa moyoni. Ni kitu kinachofanywa na Roho, na hakifanyiki ili kufuata sheria iliyoandikwa. Na yeyote aliyetahiriwa moyoni kwa Roho hupata sifa kutoka kwa Mungu, siyo kutoka kwa watu. Je, Wayahudi wana upendeleo wowote kuliko wengine? Je, tohara yao inawasaidia lolote jema? Ndiyo, Wayahudi wana upendeleo mwingi. Lililo muhimu zaidi ni kuwa: Mungu aliwaamini akawapa kazi ya kuzitangaza ahadi zake kwa watu wote. Ni kweli kuwa baadhi ya Wayahudi hawakuwa waaminifu kufanya yale Mungu aliyotaka. Lakini je, hilo laweza kumzuia Mungu kutenda kwa uaminifu yale aliyoahidi? Hapana! Hata ikiwa wengine wote watashindwa kutimiza ahadi zao, daima, Mungu atatekeleza aliyosema. Kama Maandiko yanavyosema kuhusu Mungu, “Utathibitika kuwa mwenye haki kwa maneno yako, na utashinda utakaposhitakiwa na watu.” Lakini hivi ndivyo wengine hufikiri: Tunapotenda mabaya, inaonesha wazi kuwa Mungu ni wa haki. Je, tunaweza kusema kwamba Mungu hatutendei haki anapotuadhibu? Hapana. Ikiwa Mungu si wa haki atawezaje kuuhukumu ulimwengu? Ninaposema uongo, inamletea Mungu utukufu, kwa sababu uongo wangu hurahisisha ionekane kuwa yeye ni wa kweli. Hivyo kwa nini nihukumiwe kama mtenda dhambi? Na kwa nini tusiseme, “Tufanye maovu ili jambo jema litokee humo.” Baadhi ya watu wanadai kuwa hivyo ndivyo tunavyofundisha! Wahukumiwe kwa kusema hivyo. Je, sisi Wayahudi ni bora kuliko wengine? Hapana, nimekwishaonyesha kuwa watu wote, wawe Wayahudi au wasio Wayahudi, wako chini ya nguvu ya dhambi. Kama Maandiko yanavyosema, “Hakuna atendaye haki, hakuna hata mmoja. Hakuna hata mmoja anayeelewa, hakuna anayetaka kumfuata Mungu. Wote wamegeuka na kumwacha, na hawana manufaa kwa yeyote. Hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja.” “Maneno yao ni ya hatari kama kaburi lililo wazi. Wanatumia ndimi zao kwa kusema uongo.” “Maneno yao ni kama sumu ya nyoka.” “Midomo yao imejaa maneno ya laana na hasira.” “Nyakati zote wako tayari kuua mtu. Kila wanakokwenda wanasababisha matatizo na uharibifu. Hawajui jinsi ya kuishi kwa amani.” “Hawamheshimu wala kumcha Mungu.” Tunajua ya kwamba, kile ambacho sheria inasema ni kwa ajili ya wale waliopewa sheria. Hii inamaanisha kuwa watu wote, Wayahudi na wasio Wayahudi, hawana udhuru kwa matendo yao. Hivyo ulimwengu wote unasimama mbele za Mungu na lazima ujibu kwake. Kwa sababu kufuata sheria hakumfanyi mtu akahesabiwa haki mbele za Mungu. Sheria inatuonyesha dhambi zetu tu. Lakini sasa Mungu ametuonesha jinsi alivyo mwema na mwaminifu. Alivyofanya haihusiani na sheria ingawa sheria na manabii walisema kuwa haya yangetokea. Uaminifu wa wema wa Mungu umedhihirishwa kwetu kupitia imani katika Yesu Kristo. Hufanya hivi kwa wote wanaomwamini Kristo. Kwa sababu kwa Mungu watu wote ni sawa. Ndiyo, watu wote wametenda dhambi na wameshindwa kufikia kiwango cha utukufu wa Mungu kilichokusudiwa kwao. Mungu ameamuru sisi sote tufunguliwe kutoka dhambini. Zawadi hii ya neema yake imekuja kwetu kupitia kile ambacho Kristo Yesu alikifanya ili tuwe huru. Mungu alimtoa Yesu kama njia ya kusamehe dhambi za watu kupitia imani katika yeye. Mungu anasamehe watu kwa sababu sadaka ya damu ya Yesu iliwaweka huru na dhambi zao. Mungu alimtoa Yesu kuonesha kuwa hutenda haki na bila upendeleo. Alikuwa sahihi huko nyuma alipovumilia na hakuwaadhibu watu kwa sababu ya dhambi zao. Na katika wakati wetu bado anatenda haki. Mungu alifanya hili ili awahukumu watu pasipo kuwa na upendeleo na kumwesabia haki mtu yeyote aliye na imani katika Yesu. *** Hivyo, sisi Wayahudi tuna nini cha kujivunia? Hatuna kitu. Mungu amefunga mlango kuzuia nje kiburi cha Kiyahudi. Sheria gani husema hivyo? Sheria inayohimiza matendo? Hapana, ni sheria inayosisitiza imani. Ninamaanisha kuwa watu hufanyika wenye haki na kukubaliwa na Mungu kwa njia ya imani, siyo kwa sababu ya yale wanayotenda ili kuifuata sheria. Hili ndilo tunaloamini. Je, mnadhani kuwa Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Je, yeye si Mungu wa watu wengine pia? Ndiyo, yeye ni Mungu wa wasio Wayahudi pia. Kuna Mungu mmoja tu. Atawahesabia haki Wayahudi kwa imani yao, na atawahesabia haki wasio Wayahudi kwa imani yao. Je, mnadhani kuwa tunaondoa sheria na kuweka imani hii? Hapana! Kwa kuifuata njia ya imani tunafanya kilichokusudiwa na sheria. Basi tuseme nini kuhusu Ibrahimu, baba wa watu wetu? Ikiwa Ibrahimu alifanywa kuwa mwenye haki kutokana na matendo yake, hicho ni kitu cha kujivunia! Lakini kama Mungu aonavyo, hakuwa na sababu ya kujivuna. Hili ni wazi kama Maandiko yanavyosema, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na kwa sababu ya kuamini kwake, Mungu alimhesabu kuwa mwenye haki.” Watu wanapofanya kazi, mshahara wao hautolewi kama zawadi. Ni kitu wanachopata kutokana na kazi waliyofanya. Lakini watu hawawezi kufanya kazi yoyote itakayowafanya wahesabiwe kuwa wenye haki mbele za Mungu. Hivyo ni lazima wamtumaini Yeye. Kisha huikubali imani yao na kuwahesabia haki. Yeye ndiye anayewahesabia haki hata waovu. Daudi alisema mambo hayo hayo alipozungumzia baraka wanazopata watu pale Mungu anapowahesabia haki pasipo kuangalia matendo yao: “Ni heri kwa watu wanaposamehewa kutokana na mabaya waliyotenda, dhambi zao zinapofutwa! Ni heri kwa watu, Bwana anapozifuta dhambi zao kutoka katika kumbukumbu yake!” Je, baraka hii ni kwa ajili ya waliotahiriwa tu? Au pia ni kwa ajili ya wale wasiotahiriwa? Tumekwisha sema ya kwamba Ibrahimu alikubaliwa kuwa ni mwenye haki mbele za Mungu kutokana na imani yake. Sasa katika mazingira gani hili lilitokea? Je, Mungu alimkubali Ibrahimu na kumhesabia haki kabla au baada ya kutahiriwa? Mungu alimkubali kabla ya kutahiriwa kwake. Ibrahimu alitahiriwa baadaye ili kuonesha kuwa Mungu amemkubali kuwa mwenye haki. Tohara yake ilikuwa uthibitisho kwamba Mungu alimhesabia haki kwa njia ya imani hata kabla ya kutahiriwa. Hivyo Ibrahimu ni baba wa wote wanaoamini lakini hawajatahiriwa. Kama Ibrahimu, wao pia wamekubaliwa na Mungu kuwa wenye haki kwa sababu ya imani yao tu. Pia Ibrahimu ni baba wa waliotahiriwa, lakini si kwa sababu ya kutahiriwa kwao. Ni baba yao kwa sababu wao nao wamemwamini Mungu vile vile kama Ibrahimu alivyofanya kabla hajatahiriwa. Mungu aliweka ahadi kwa Ibrahimu na wazaliwa wake ya kuwapa ulimwengu wote. Lakini kwa nini Mungu aliweka ahadi hii? Haikuwa kwa sababu Ibrahimu aliifuata sheria. Ni kwa sababu aliiweka imani yake katika Mungu na akakubaliwa kuwa mwenye haki. Watu wa Mungu watarithi yote ambayo Mungu alimwahidi Ibrahimu, lakini si kwa sababu wanaifuata sheria. Ikiwa ni lazima tuitii sheria ili tupate kile alichoahidi Mungu, badi imani ya Ibrahimu haina maana yoyote na ahadi ya Mungu haina manufaa. Ninasema hivi kwa sababu sheria ndiyo huleta hasira ya Mungu kwa wale wasioitii. Lakini ikiwa sheria haipo, basi hakuna hatia ya kutoitii. Hivyo watu hupokea ahadi ya Mungu kwa imani. Hili hutokea ili ahadi hiyo iwe kipawa cha bure. Na ikiwa ahadi ni kipawa cha bure, basi watu wote wa Ibrahimu watapata ahadi hiyo. Ahadi hii si tu kwa ajili ya wale wanaoishi chini ya Sheria ya Musa. Bali ni kwa ajili ya wote wanaoishi kwa kuweka imani yao kwa Mungu kama Ibrahimu alivyofanya. Ni baba yetu sote. Kama Maandiko yanavyosema, “Nimekufanya uwe baba wa mataifa mengi.” Ibrahimu aliposikia ahadi hii, aliiweka imani yake kwa Mungu. Mungu ndiye awapaye uhai waliokufa na kwa amri yake huumba kisichokuwepo. Halikuwepo tumaini kwamba Ibrahimu angepata watoto, lakini alimwamini Mungu na akaendelea kutumaini. Na ndiyo sababu akafanyika kuwa baba wa mataifa mengi. Kama Mungu alivyomwambia kuwa, “Utakuwa na wazaliwa wengi.” Ibrahimu alikuwa na umri uliokaribia miaka 100, hivyo alikuwa amevuka umri wa kupata watoto. Pia, Sara hakuweza kuwa na watoto. Ibrahimu alilijua hili vizuri, lakini imani yake kwa Mungu haikudhoofika. Hakutilia shaka kuwa Mungu angetenda kile alichoahidi. Hakuacha kuamini. Kwa hakika, aliendelea kuimarika katika imani yake. Alitukuza Mungu na alikuwa na uhakika kuwa Mungu anaweza kutenda alichoahidi. Ndiyo sababu “Mungu alimkubali kuwa ni mwenye haki”. Maneno haya, “alikubaliwa”, yaliandikwa siyo tu kwa ajili ya Ibrahimu. Pia yaliandikwa kwa ajili yetu. Mungu atatukubali sisi pia kwa sababu tunaamini. Tunamwamini yule aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu. Yesu alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, na akafufuliwa kutoka kifo ili Mungu atuhesabie haki. Tumehesabiwa haki mbele za Mungu kwa njia ya imani. Hivyo sote tuna amani pamoja na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kupitia imani yetu, Kristo ametufungulia mlango kuingia katika neema ya Mungu, tunayoifurahia sasa. Na tunashangilia sana kwa sababu ya tumaini tulilonalo la kushiriki utukufu wa Mungu. Na tunafurahia matatizo tunayoyapitia. Kwa nini? Kwa sababu tunajua kuwa mateso hutufundisha kuwa jasiri kipindi kigumu. Na ujasiri huu ni uthibitisho kuwa tuko imara. Na uthibitisho huu unatupa tumaini. Na tukiwa na tumaini hili, hatutakata tamaa kamwe. Tunajua hili kwa sababu Mungu ameumimina upendo wake na kuijaza mioyo yetu kupitia Roho Mtakatifu aliyetupa. Yote haya ni kweli kutokana na aliyoyafanya Kristo. Wakati sahihi ulipotimia, tukiwa hatuwezi kujisaidia wenyewe na tusioonyesha heshima yoyote kwa Mungu, yeye Kristo, alikufa kwa ajili yetu. Ni watu wachache walio tayari kufa ili kuokoa maisha ya mtu mwingine, hata kama mtu huyo ni mwema. Mtu anaweza kuwa radhi kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema sana. Lakini Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa bado ni wenye dhambi, na kwa hili Mungu akatuonyesha jinsi anavyotupenda sana. Tumehesabiwa haki mbele za Mungu kwa sababu ya sadaka ya damu ya Kristo. Hivyo kwa njia ya Kristo hakika tutaokolewa kutoka katika ghadhabu ya Mungu. Nina maana kuwa tulipokuwa bado adui wa Mungu, Yeye alifanya urafiki nasi kwa njia ya kifo cha Mwanaye. Kutokana na ukweli kwamba sasa tumekuwa marafiki wa Mungu, basi tunaweza kupata uhakika zaidi kwamba Baba atatuokoa kupitia uhai wa Mwanaye. Na si kuokolewa tu, bali pia, hata sasa tunafurahi kwa yale ambayo Mungu ametutendea kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kwa sababu ya Yesu sisi ni marafiki wa Mungu sasa. Dhambi ilikuja ulimwenguni kwa sababu ya kile alichofanya mtu mmoja. Na dhambi ikaleta kifo. Kwa sababu hiyo ni lazima watu wote wafe, kwa kuwa watu wote wametenda dhambi. Dhambi ilikuwepo ulimwenguni kabla ya Sheria ya Musa. Lakini Mungu hakutunza kumbukumbu ya dhambi ya watu wakati sheria haikuwepo. Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Musa, mauti ilitawala juu ya kila mtu. Adamu alikufa kwa sababu alitenda dhambi kwa kutokutii amri ya Mungu. Lakini hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa njia hiyo hiyo walipaswa kufa. Hivyo mtu mmoja Adamu anaweza kufananishwa na Kristo, Yeye ambaye angekuja baadaye. Lakini kipawa cha Mungu hakifanani na dhambi ya Adamu. Watu wengi walikufa kwa sababu ya dhambi ya mtu huyo mmoja. Lakini neema waliyopokea watu kutoka kwa Mungu ilikuwa kuu zaidi. Wengi walikipokea kipawa cha Mungu cha uzima kwa neema ya huyu mtu mwingine, Yesu Kristo. Baada ya Adamu kutenda dhambi mara moja, alihukumiwa kuwa na hatia. Lakini kipawa cha Mungu ni tofauti. Kipawa chake cha bure kilikuja baada ya dhambi nyingi, nacho kinawafanya watu wahesabiwe haki mbele za Mungu. Mtu mmoja alitenda dhambi, hivyo kifo kikawatawala watu wote kwa sababu ya huyo mtu mmoja. Lakini sasa watu wengi wanaipokea neema ya Mungu iliyo nyingi sana na karama yake ya ajabu ya kufanyika wenye haki. Hakika watakuwa na uzima wa kweli na kutawala kupitia mtu mmoja, Yesu Kristo. Hivyo dhambi hiyo moja ya Adamu ilileta adhabu ya kifo kwa watu wote. Lakini kwa njia hiyo hiyo, Kristo alifanya kitu chema zaidi kilichowezesha watu kufanyika wenye haki mbele za Mungu. Na hicho huwaletea uzima wa kweli. Mtu mmoja hakumtiii Mungu na wengi wakafanyika wenye dhambi. Lakini kwa namna hiyo hiyo, mtu mmoja alipotii, wengi wamefanyika kuwa wenye haki. Baada ya sheria kuja, zilikuwepo njia nyingi za watu kufanya makosa. Lakini kadri watu walivyozidi kufanya dhambi, ndivyo Mungu alivyomimina zaidi neema yake. Hapo kale dhambi ilitumia kifo kututawala. Lakini sasa neema ya Mungu inatawala juu ya dhambi na kifo kwa sababu ya wema wake wenye uaminifu. Na hii inatuletea maisha ya milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu. Hivyo, je, mnadhani inatupasa tuendelee kutenda dhambi ili Mungu atupe neema nyingi zaidi na zaidi? Hapana! Utu wetu wa zamani wa dhambi ulikwisha. Umekufa. Je, tutaendeleaje kuishi katika dhambi? Je, mmesahau kwamba sisi sote tulifanyika sehemu ya Kristo Yesu tulipobatizwa? Katika ubatizo wetu tulishiriki katika kifo chake. Hivyo, tulipobatizwa, tulizikwa pamoja na Kristo na kushiriki katika kifo chake. Na kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa nguvu ya ajabu ya Baba, ndivyo nasi tunaweza kuishi maisha mapya sasa. Kristo alikufa, nasi tumeunganishwa pamoja naye kwa kufa kama yeye alivyokufa. Kwa hiyo tutaunganishwa pamoja naye kwa kufufuka kutoka katika kifo kama yeye alivyofanya. Tunajua kuwa utu wetu wa zamani ulikufa msalabani pamoja naye. Hivyo ndivyo maisha ya utumwa tuliyokuwa nayo yalivyoangamizwa ili tusiendelee kuitumikia dhambi tena. Yeyote aliyekufa amewekwa huru kutoka katika nguvu za dhambi. Ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunajua kwamba tutaishi pamoja naye pia. Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na tunajua kuwa hawezi kufa tena. Sasa mauti haina nguvu juu yake. Ndiyo, Kristo alipokufa, alikufa ili aishinde nguvu ya dhambi mara moja, na siyo mara nyingine tena. Sasa anao uzima mpya, na uzima wake huo upo kwa nguvu za Mungu. Kwa namna hiyo hiyo, mnapaswa kujiona kama mliokufa kwa dhambi na mlio hai kwa nguvu za Mungu kupitia Kristo Yesu. Mwili mlionao katika uhai wenu wa sasa hapa duniani utakufa. Msiruhusu dhambi iutawale na kuwafanya ninyi kuzitumikia tamaa zake. Msiitoe sehemu ya miili yenu kwa dhambi kwa ajili ya kutumika kutenda maovu. Jitoeni kwa Mungu, kama watu waliokufa lakini walio hai. Toeni sehemu za miili yenu kwa Mungu ili zitumiwe kwa kutenda mema. Dhambi haitakuwa mtawala wenu, kwa sababu hamko chini ya sheria. Sasa mnaishi chini ya neema ya Mungu. Hivyo tufanye nini? Je, tutende dhambi kwa sababu tuko chini ya neema na siyo chini ya sheria? Hapana! Hakika mnajua kuwa unakuwa mtumwa wa jambo lolote unaojitoa kulifanya. Chochote au yeyote unayemtii atakuwa bwana wako. Unaweza kufuata dhambi, au kumtii Mungu. Kufuata dhambi kunaleta kifo cha kiroho, lakini kumtii Mungu kunakufanya uhesabiwe na Mungu. Hapo zamani mlikuwa watumwa wa dhambi na dhambi iliwatawala. Lakini ashukuriwe Mungu, mlitii kwa hiyari mafundisho yote aliyowaelekeza. Mliwekwa huru kutoka katika dhambi, na sasa ninyi ni watumwa wa uaminifu wa wema wa Mungu. Natumia dhana hii ya utumwa kutoka katika maisha ya kila siku kwa sababu mnahitaji msaada katika kuielewa kweli hii ya kiroho. Zamani mliitoa sehemu ya miili yenu kuwa watumwa wa mawazo yenu yaliyo machafu na maovu. Matokeo yake mliishi kwa ajili ya dhambi tu. Kwa njia hiyo hiyo, sasa mnapaswa kujitoa wenyewe kama watumwa wa uaminifu wa wema wa Mungu ili mweze kufaa kabisa kwa utumishi kwake. Zamani mlikuwa watumwa wa dhambi, na wala hamkufikiri juu ya kutenda haki. Mlifanya mambo maovu, na sasa mnaaibishwa kwa yale mliyotenda. Je, mambo haya yaliwasaidia? Hapana, yalileta kifo tu. Lakini sasa mko huru dhidi ya dhambi. Mmekuwa watumwa wa Mungu, na mnaishi kwa ajili ya Mungu tu. Hili litawaletea uzima wa milele. Watu wanapotenda dhambi, wanapokea malipo ya dhambi, ambayo ni kifo. Lakini Mungu huwapa watu wake zawadi ya bure, yaani uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu. Ndugu zangu, ninyi nyote mnailewa sheria ya Musa. Hivyo kwa hakika mnafahamu kuwa sheria huwatawala watu wanapokuwa hai tu. Ni kama ambavyo sheria kuhusu ndoa inavyosema: ni lazima mwanamke abaki katika ndoa mume wake akiwa hai. Lakini mume wake akifa, atakuwa amewekwa huru kutoka katika sheria ya ndoa. Iwapo ataolewa na mwanaume mwingine, mume wake akiwa angali hai, sheria inasema kuwa ana hatia ya uzinzi. Lakini mumewe akifa, atakuwa amewekwa huru kutoka katika sheria ya ndoa. Hivyo akiolewa na mwanaume mwingine baada ya mumewe kufa, hatakuwa na hatia ya uzinzi. Kwa njia hiyo hiyo, kaka na dada zangu, mliwekwa huru kutoka katika sheria utu wenu wa zamani ulipokufa pamoja na Kristo. Sasa ninyi ni mali yake yeye yule aliyefufuliwa kutoka kwa wafu. Sote ni mali ya Kristo ili tutumike kwa ajili ya huduma kwa Mungu. Hapo zamani tulitawaliwa na udhaifu wetu wa kibinadamu. Sheria ilitufanya tutake kutenda dhambi. Na tamaa hizo za dhambi ziliitawala miili yetu, na yale tuliyofanya yalituletea mauti ya rohoni. Sasa, kama watu waliokufa, tuko huru kutoka katika sheria iliyotushikilia kama wafungwa. Hivyo hatumtumikii Mungu tena kwa jinsi ya zamani, kwa sheria zilizoandikwa. Sasa tunamtumikia Mungu kwa namna mpya, kwa Roho. Mnaweza kudhani ninasema ya kwamba dhambi na sheria vinafanana. Sisemi hivyo. Lakini sheria ilikuwa njia pekee ya kunifundisha maana ya dhambi. Nisingeweza kujua kwamba ni kosa kutamani kitu kisichokuwa changu. Lakini sheria inasema, “Usitamani mali ya mtu mwingine.” Na dhambi kwa kutumia amri hiyo, ikanifanya nitamani kila kitu kisichokuwa changu. Hivyo dhambi ilikuja kwangu kutokana na amri hiyo. Lakini bila sheria, dhambi imekufa na haina nguvu. Kabla sijaijua sheria, nilikuwa hai. Lakini nilipoijua sheria, dhambi ikaanza kuishi ndani yangu, na hiyo ikawa na maana ya kifo kwangu. Amri ilikusudiwa kuleta uzima, lakini kwangu iliniletea kifo. Dhambi ilipata njia ya kunidanganya kwa kutumia amri ili nife. Hivyo, sheria ni takatifu na amri ni takatifu, sahihi na nzuri. Je, hii ina maana kuwa kitu ambacho ni kizuri kiliniletea kifo? Hapana, ni dhambi iliyoitumia amri nzuri ndiyo iliyoniletea kifo. Hii inaonesha kwa hakika kuwa dhambi ni dhambi. Dhambi inaweza kutumia amri iliyo nzuri na kuleta matokeo yanayoonesha ubaya wake mkubwa. Tunafahamu kuwa sheria ni ya rohoni, lakini mimi si wa rohoni. Mimi ni mwanadamu hasa. Dhambi inanitawala kana kwamba mimi ni mtumwa wake. Sielewi ni kwa nini ninatenda jinsi ninavyotenda. Sitendi mema ninayotaka kuyatenda, bali ninatenda maovu ninayoyachukia. Na ikiwa ninatenda kile nisichotaka kutenda, inamaanisha kuwa ninakubali kuwa sheria ni njema. Lakini kwa hakika siyo mimi mwenyewe ninayetenda maovu. Bali dhambi inayokaa ndani yangu ndiyo inatenda hayo. Ndiyo, ninajua kuwa hakuna kitu chema kinachoishi ndani yangu, nina maana kuwa hakuna kitu chema kinachoishi ndani yangu kisichokuwa cha rohoni. Sitendi mema ninayotaka nitende. Ninatenda maovu nisiyotaka kutenda. Hivyo ikiwa ninatenda yale nisiyotaka kutenda, hakika si mimi ninayeyatenda hayo. Bali dhambi inayoishi ndani yangu ndiyo inayotenda. Hivyo nimejifunza hivi kuhusu sheria: Ninapotaka kutenda mema ambayo sheria inaamrisha, uovu unakuwa hapo hapo pamoja nami. Moyoni mwangu nafurahi kuifuata sheria ya Mungu. Lakini naiona “sheria” nyingine ikitenda kazi ndani yangu, nayo imo vitani dhidi ya sheria inayokubalika akilini mwangu. “Sheria” hii nyingine ni utawala wa dhambi inayonishinda na inanifanya kuwa mfungwa wake. Mimi ni mtu mwenye taabu kiasi gani! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu unaoniletea kifo? Namshukuru Mungu kwa wokovu wake kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo katika ufahamu wangu mimi ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika udhaifu wangu wa kibinadamu mimi ni mtumwa wa sheria ya dhambi. Hivyo mtu yeyote aliye wa Kristo Yesu hana hukumu ya kifo. Hiyo ni kwa sababu kwa njia ya Kristo Yesu sheria ya Roho inayoleta uzima imewaweka ninyi huru kutoka katika sheria inayoleta dhambi na kifo. Ndiyo, sheria haikuwa na nguvu ya kutusaidia kwa sababu ya udhaifu wetu wa kibinadamu. Lakini Mungu akafanya kile ambacho sheria haikuweza kufanya: Alimtuma Mwanaye duniani akiwa na mwili ule ule tunaoutumia kutenda dhambi. Mungu alimtuma ili awe njia ya kuiacha dhambi. Alitumia maisha ya mwanadamu ili kuipa dhambi hukumu ya kifo. Mungu alifanya hivi ili tuweze kuishi kama sheria inavyotaka. Sasa tunaweza kuishi hivyo kwa kumfuata Roho na si kwa jinsi ya udhaifu wa kibinadamu. Watu wanaoishi kwa kufuata udhaifu wa kibinadamu huyafikiri yale wanayoyataka tu. Lakini wale wanaoishi kwa kumfuata Roho huyafikiri yale Roho anayotaka wafanye. Ikiwa fikra zenu zinaongozwa na udhaifu wa kibinadamu, kuna kifo cha kiroho. Lakini ikiwa fikra zenu zinaongozwa na Roho, kuna uhai na amani. Je, hili ni kweli? Kwa sababu kila mtu ambaye fikra zake zinaongozwa na udhaifu wa kibinadamu yuko kinyume na Mungu maana hukataa kuitii sheria ya Mungu. Na kwa hakika hawawezi kutii. Wale wanaotawaliwa na udhaifu wa kibinadamu hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ninyi hamtawaliwi na udhaifu wenu wa kibinadamu, bali mnatawaliwa na Roho, ikiwa Roho huyo wa Mungu anakaa ndani yenu. Na mtu yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wa Kristo. Miili yenu inaelekea kifo kwa sababu ya dhambi. Lakini ikiwa Kristo anaishi ndani yenu, basi Roho anawapa uzima kwa sababu ya uaminifu wa wema wa Mungu. Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Na ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu, ataifanya hai tena miili yenu inayokufa. Ndiyo, Mungu ndiye aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu, naye atawafufua ninyi na kuwapa uzima kupitia Roho wake anayeishi ndani yenu. Hivyo, kaka na dada zangu, ni lazima tusitawaliwe na udhaifu wa kibinadamu kwa kufuata tamaa zake. Ikiwa mtayatumia maisha yenu kufanya yale ambayo udhaifu wenu wa kibinadamu unataka, mtakufa kiroho. Lakini ikiwa mtaupokea msaada wa Roho na mkaacha kutenda mambo mabaya mnayotenda na miili yenu, mtakuwa na uzima wa kweli. Watoto wa kweli wa Mungu ni wale wanaokubali kuongozwa na Roho wa Mungu. Roho tuliyempokea si roho anayetufanya kuwa watumwa tena na kutusababisha tuwe na hofu. Roho tuliye naye hutufanya tuwe watoto waliochaguliwa na Mungu. Na kwa Roho huyo twalia “ Aba, yaani Baba.” Na Roho mwenyewe huzungumza na roho zetu na kutuhakikishia kuwa sisi ni watoto wa Mungu. Nasi kwa kuwa ni watoto wa Mungu, basi sisi ni warithi, warithi wa Mungu na warithi pamoja na Kristo. Mungu atatupa yale yote aliyompa Kristo. Sisi tunaoteseka sasa kama Kristo alivyoteseka tutashiriki katika utukufu wake. Nanayachukulia mateso ya sasa kuwa si kitu ukilinganisha na utukufu mkuu tunaoutarajia. Hata uumbaji una shauku kuu, ukisubiri kwa hamu wakati ambapo atawadhihirisha “watoto halisi wa Mungu” kuwa ni na. Kila alichokiumba Mungu kiliruhusiwa kuwa na mapungufu kana kwamba hakitafikia utimilifu wake. Hilo halikuwa kwa matakwa ya viumbe, lakini Mungu aliruhusu hayo yatokee kwa mtazamo wa tumaini hili: kwamba uumbaji ungewekwa huru mbali na uharibifu, na kwamba kila alichokiumba Mungu kiwe na uhuru na utukufu ule ule ulio wa watoto wa Mungu. Tunajua kuwa kila kitu alichoumba Mungu kimekuwa kikingoja hadi sasa katika kuugua na uchungu kama wa mwanamke aliye tayari kuzaa mtoto. Siyo uumbaji tu, bali sisi pia tumekuwa tukingoja kwa kuugua na uchungu ndani yetu. Tunaye Roho kama sehemu ya kwanza ya ahadi ya Mungu. Kwa hiyo tunamngoja Mungu amalize kutufanya sisi watoto wake yeye mwenyewe. Nina maana kuwa tunasubiri kuwekwa huru kwa miili yetu. Tuliokolewa ili tuwe na tumaini hili. Ikiwa tunaweza kuona kile tunachokisubiri, basi hilo siyo tumaini la kweli. Watu hawatumaini kitu ambacho tayari wanacho. Lakini tunatumaini kitu tusichokuwa nacho, na hivyo tunakisubiri kwa uvumilivu. Roho hutusaidia pia. Sisi ni dhaifu sana, lakini Roho hutusaidia katika udhaifu wetu. Hatujui jinsi ya kuomba kama Mungu anavyotaka, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa Mungu kwa kuungua kusikotamkika. Tayari Mungu anayajua mawazo yetu ya ndani sana. Na anaelewa Roho anataka kusema nini, kwa sababu Roho huomba kwa ajili ya watu wa Mungu katika namna inayokubaliana na mapenzi ya Mungu. Tunajua kwamba katika kila kitu Mungu hufanya kazi ili kuwapa mema wale wanaompenda. Hawa ni watu aliowachagua Mungu, kwa sababu huo ndiyo ulikuwa mpango wake. Mungu aliwajua kabla hajauumba ulimwengu. Na aliamua hao wangekuwa kama Mwanaye. Na Yesu angekuwa mzaliwa wa kwanza wa watoto wake wengi. Mungu aliwakusudia wao wawe kama Mwanaye. Aliwachagua na kuwahesabia haki pamoja na Mungu. Na alipowahesabia haki, akawapa utukufu wake. Hivyo tuseme nini juu ya hili? Ikiwa Mungu yuko kwa ajili yetu, hakuna anayeweza kuwa kinyume nasi. Naye alimwacha mwanae ateswe kwa ajili yetu. Mungu alimtoa Mwanaye kwa ajili yetu sisi sote. Sasa kwa kuwa tu wa Kristo, hakika Mungu atatupa mambo mengine yote. Nani atakayewashitaki watu waliochaguliwa na Mungu? Hayupo! Mungu ndiye hutuhesabia haki. Ni nani anaweza kuwahukumu watu wa Mungu kuwa wana hatia? Hayupo! Kristo Yesu alikufa kwa ajili yetu na alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na sasa ameketi upande wa kulia wa Mungu na anazungumza na Mungu kwa ajili yetu. Je, kuna kitu chochote kinachoweza kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni matatizo au shida au mateso? Ikiwa hatuna chakula au mavazi au tunakabiliwa na hatari au kifo, je mambo hayo yatatutenga sisi kutoka katika upendo wake? Kama Maandiko yanavyosema, “Kwa ajili yako, tunakabiliana na kifo wakati wote. Watu wanadhani hatuna thamani kama kondoo wanaowachinja.” Lakini katika shida zote hizo tuna ushindi kamili kupitia Mungu, aliyetuonyesha upendo wake. Ndiyo, nina uhakika kuwa hakuna kitu kinachoweza kututenganisha sisi na upendo wa Mungu, si kifo, maisha, malaika, wala roho zinazotawala. Nina uhakika kuwa hakuna wakati huu, hakuna wakati ujao; hakuna mamlaka, hakuna kilicho juu yetu au chini yetu, hakuna katika ulimwengu wote ulioumbwa, kitakachoweza kututenganisha sisi na upendo wa Mungu ulioonyeshwa kwetu katika Kristo Yesu Bwana wetu. Nazungumza nayi sasa kama mmojawapo niliye wa Kristo. Hivyo mnaweza kuwa na uhakika kuwa sisemi uongo. Dhamiri yangu, inayotawaliwa na Roho Mtakatifu, inakubali kwamba ninayowaambia sasa ni kweli. Nimejawa na huzuni na maumivu ya moyoni yasiyokwisha kwa ajili ya watu wangu. Wao ni kaka na dada zangu katika mwili. Natamani ningeweza kuwasaidia. Ningekuwa tayari pia kuomba kupokea laana ya kutengwa na Kristo kama hiyo itaweza kuwasaidia. Ni Waisraeli, watoto waliochaguliwa na Mungu. Wameushuhudia utukufu wa Mungu na wanashiriki maagano aliyofanya Mungu na watu wake. Mungu aliwapa Sheria ya Musa, ibada ya Hekalu, na ahadi zake. Ni wazaliwa wa mababa zetu wakuu, na ni familia ya kidunia ya Masihi, ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote. Yeye asifiwe milele! Amina. Sina maana kuwa Mungu alishindwa kutimiza ahadi yake kwa Wayahudi. Lakini kwa hakika ni baadhi tu ya Waisraeli ndiyo watu wa Mungu. Na hivyo ni baadhi tu ya watoto wa Ibrahimu ndiyo wazaliwa wake halisi. Hivi ndivyo Mungu alimwambia Ibrahimu: “Wazaliwa wako halisi watakuwa wale waliotoka kwa Isaka.” Hii ina maana kuwa si watoto wote wa Ibrahimu walio watoto halisi wa Mungu. Wazaliwa halisi wa Ibrahamu ni wale wanaofanyika watoto wa Mungu kwa sababu ya agano ambalo Mungu alililiweka na Ibrahamu. Hivi ndivyo Mungu alivyosema katika agano hilo: “Wakati kama huu mwaka ujao nitakujia tena, na Sara mke wako atazaa mwana.” Na si hivyo tu. Kitu kama hicho kilimtokea Rebeka ambaye baada ya kupata mimba ya wana wawili mapacha waliotokana na baba mmoja, baba yetu Isaka. Ndiyo, kabla ya kuzaliwa wana hao mapacha, Mungu alimwambia Rebeka, “Mwana mkubwa atamtumikia mdogo.” Hii ilikuwa kabla wavulana hawa hawajatenda jambo lolote jema au baya. Mungu alisema hivi kabla hawajazaliwa ili kwamba mvulana ambaye Mungu alimtaka atachaguliwa kutokana na mpango wa Mungu mwenyewe. Mvulana huyu alichaguliwa kwa sababu ndiye ambaye Mungu alitaka kumwita, si kwa sababu ya jambo lolote walilofanya wavulana hao. *** Kama Maandiko yanavyosema, “Nilimpenda Yakobo lakini nilimchukia Esau.” Namsikia mtu akiuliza, “Hivyo hii ina maana gani? Je, Mungu si mwenye haki?” Hapana! Mungu alimwambia Musa, “Nitampa rehema yeyote ninayetaka kumpa rehema. Nitamhurumia yeyote ninayemchagua.” Hivyo Mungu atamchagua yeyote anayeamua kumpa rehema pasipo kujali watu wanataka nini ama kwa jinsi gani wanapiga mbio. Katika Maandiko Mungu anamwambia Farao: “Nilikuweka uwe mfalme kwa kusudi hili hasa: kuonesha nguvu zangu kupitia kwako. Nilitaka jina langu litangazwe ulimwenguni kote” Hivyo Mungu huwarehemu wale anaotaka kuwarehemu na huwafanya jeuri wale anaotaka wawe jeuri. Hivyo utaniuliza, “Ikiwa unayosema ni kweli, kwa nini Mungu amlaumu mtu yeyote kwa kufanya makosa? Hayupo anayeweza kukataa kufanya yale anayotaka Mungu, Je, yupo?” Hilo si la kuuliza. Wewe ni mwanadamu tu na huna haki ya kumhoji Mungu. Chungu hakiwezi kumhoji aliyekifinyanga. Hakiwezi kusema, “Kwa nini ulinifinyanga hivi?” Yeye aliyefinyanga chungu anaweza kufinyanga kitu chochote anachotaka. Anautumia udongo ule ule wa mfinyanzi kufinyanga vitu mbalimbali. Anaweza kufinyanga kitu kimoja kwa makusudi maalumu na kingine kwa matumizi ya kila siku. Ni kwa jinsi hiyo hiyo Mungu amefanya. Alitaka kuionesha hasira yake na kuwafanya watu waone nguvu zake. Lakini kwa uvumilivu wake aliwastahimili wale waliomuudhi, watu waliokuwa tayari kuangamizwa. Alingoja kwa uvumilivu ili aweze kuutangaza utajiri wa utukufu wake kwa watu aliowachagua wapokee rehema zake. Mungu alikwisha waandaa kuushiriki utukufu wake. Sisi ndiyo watu hao, ambao Mungu alituchagua si tu kutoka kwa Wayahudi lakini pia kutoka kwa wale wasio Wayahudi. Kama Mungu anavyosema katika kitabu cha Hosea, “Watu wasiokuwa wangu, nitasema ni watu wangu. Na watu ambao sikuwapenda, nitasema ni watu ninaowapenda. Na pale Mungu aliposema zamani: ‘Ninyi si watu wangu’; hapo wataitwa watoto wa Mungu aliye hai.” Na Isaya huililia Israeli: “Wako watu wengi sana wa Israeli, kuliko mchanga ulio pwani ya baharini. Lakini wachache wao watakaookolewa. Ndiyo, Bwana atakamilisha kwa haraka aliyosema atayafanya duniani.” Ni kama vile alivyosema Isaya: “Ikiwa Bwana Mwenye Uweza wote asingewaruhusu watu wachache wakaishi, tungekuwa tumeangamizwa kabisa, kama vile miji miovu ya Sodoma, na Gomora.” Hivyo haya yote yanamaanisha nini? Je, tunasema kwamba watu wasio Wayahudi walifanikiwa kukipata kibali cha Mungu, hata kama hawakuwa wakijaribu kukipata kibali hicho? Ndiyo. Walipata kibali hicho kwa sababu ya imani kwa Mungu. Na vipi kuhusu watu wa Israeli? Wao walitaka kujipatia kibali cha Mungu kwa kuifuata sheria. Je, tunasema kuwa hawakufanikiwa? Ndiyo, na sababu yake ni hii: Walijitahidi kukipata kwa kufanya kwa usahihi mambo yote yaliyoamriwa katika sheria badala ya kumtumaini Mungu. Walijikwaa kwenye jiwe linalowafanya watu waanguke. Maandiko yanazungumza kuhusu jiwe hilo: “Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni litakalowafanya watu wajikwae. Ni mwamba utakaowaangusha watu. Lakini yeyote atakayemtumaini yeye hataaibika kamwe.” Kaka na dada zangu, ninalotamani zaidi ni kwamba Waisraeli wote waokolewe. Hayo ndiyo maombi yangu kwa Mungu. Naweza kusema hili juu yao: Kwa hakika wana bidii sana ya kumtii Mungu, lakini hawaijui njia iliyo sahihi. Hawakuelewa kile ambacho Mungu alifanya ili kuwaokoa watu. Hivyo walijaribu kwa njia yao wenyewe kupata kibali kwa Mungu kwa kuishika sheria. Na wakakataa kuifuata njia ya Mungu ya kuwaokoa watu. Sheria ilifikia mwisho wake wakati Kristo alipolikamilisha kusudi lake. Sasa kila mtu anayeiweka imani yake kwake anahesabiwa haki mbele za Mungu. Musa anaandika juu ya kuhesabiwa haki kwa kuifuata sheria. Anasema: “Ili kupata uzima katika sheria imempasa mtu kuzitii.” Lakini Maandiko yanasema haya kuhusu kuhesabiwa haki kwa njia ya imani: “Usiyaseme haya kwako wewe mwenyewe, ‘Nani atapanda kwenda mbinguni?’” (Hii inamaanisha “Nani atapanda mbinguni kumchukua Kristo na kumleta chini duniani?”) “Na usiseme, ‘Nani atashuka hadi ulimwengu uliopo chini huko?’” (Hii inamaanisha “Nani atashuka chini na kumchukua Kristo na kumfufua kutoka mauti?”) Hivi ndivyo Maandiko yanavyosema: “Mafundisho ya Mungu yako karibu nawe; yako katika kinywa chako na katika moyo wako.” Ni mafundisho ya imani tunayowaambia watu. Ukikiri wazi kwa kinywa chako, kwamba “Yesu ni Bwana” na kuamini moyoni mwako kuwa Mungu alimfufua kutoka mauti, utaokolewa. Ndiyo, tunamwamini Yesu mioyoni mwetu, na Mungu hutukubali kuwa wenye haki. Na tunakiri wazi wazi kwa vinywa vyetu kwamba tunamwamini Mungu na yeye anatuokoa. Ndiyo, Maandiko yanasema, “Yeyote anayemwamini hataaibika.” Yanasema hivi kwa sababu hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi. Bwana yule yule ndiye Bwana wa watu wote. Naye humbariki sana kila amwombaye akitaka msaada. Ndiyo, “kila mtu anayemwita Bwana ili kupata msaada, ataokolewa.” Lakini watu watawezaje kumwita Bwana na kupata msaada wake ikiwa hawamwamini yeye? Na watawezaje kumwamini Bwana ikiwa hawajawahi kuzisikia habari zake? Na watawezaje kuzisikia habari zake ikiwa hayupo mtu wa kuwaambia? Na mtu atawezaje kwenda na kuwaambia habari hizo ikiwa hajatumwa? Haya, hii ndiyo sababu Maandiko yanasema, “Ni jambo la kufurahisha kumwona mtu anayepeleka Habari Njema!” Lakini si watu wote walizipokea Habari Njema hizo. Na hii ndiyo sababu Isaya alisema, “Bwana, nani aliyeamini yale tuliyowaeleza?” Kwa hiyo imani hupatikana kutokana na kusikia Habari Njema. Na watu husikia Habari Njema wakati mtu anapowaeleza kuhusu Kristo. Lakini nauliza, “Je, watu hao walizisikia Habari Njema?” Ndio Kwa kweli walizisikia kama Maandiko yanavyosema, “Sauti zao zilitoka na kuenea duniani kote. Maneno yao yakaenda kila mahali ulimwenguni.” Lakini tena nauliza, “Je, watu wa Israeli hawakuelewa?” Ndiyo, walielewa. Musa alikuwa wa kwanza kujibu swali hili. Na anasema haya kwa ajili ya Mungu: “Nitawatumia wale ambao siyo Taifa halisi ili liwafanye muone wivu. Nitalitumia taifa ambalo halielewi ili mkasirike.” Kisha Isaya ana ujasiri wa kutosha kusema haya kwa ajili ya Mungu: “Watu walionipata mimi hawakuwa wakinitafuta. Nilijitambulisha kwa watu ambao hawakuwa wakinitafuta.” Lakini kuhusu watu wa Israeli Mungu anasema, “Kutwa nzima nilisimama nikiwa tayari kuwakubali watu hawa, lakini ni wakaidi na wamekataa kunitii.” Hivyo ninauliza, “Je, Mungu aliwakataa watu wake?” Hapana! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, wa ukoo wa Ibrahimu, katika kabila la Benjamini. Mungu aliwachagua Waisraeli wawe watu wake kabla hawajazaliwa. Na hajawakataa. Hakika mnajua Maandiko yanavyosema kuhusu Eliya anapomwomba Mungu dhidi ya watu wa Israeli. Anasema, “Bwana, wamewaua manabii wako na kuharibu madhabahu zako. Mimi ndiye nabii pekee niliyebaki hai, na sasa wanajaribu kuniua mimi pia.” Lakini ni jibu gani Mungu alilompa Eliya? Mungu alisema, “Nimejihifadhia watu elfu saba wasiomwabudu Baali.” Ndivyo ilivyo sasa. Mungu amewachagua watu wachache kwa neema yake. Na kama aliwachagua kwa neema yake, hivyo si kwa sababu ya matendo yao yaliyowafanya wawe watu wake. Kama wangefanywa kuwa watu wake kutokana na matendo yao, zawadi yake ya neema isingekuwa zawadi halisi. Hivyo hivi ndivyo ilivyotokea: Watu wa Israeli wanazitaka sana baraka za Mungu, lakini si wote waliozipata. Watu aliowachagua walipata baraka zake, lakini wengine wakawa wagumu na wakakataa kumsikiliza. Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu aliwafanya watu walale usingizi.” “Mungu aliyafumba macho yao ili wasione, na aliyaziba masikio yao ili wasisikie. Hili linaendelea hata sasa.” Na Daudi anasema, “Watu hawa na wakamatwe na kunaswa katika tafrija wanazofurahia. Nyakati hizo nzuri ziwasababishe waanguke ili wapate adhabu wanayoistahili. Yapofushe macho yao ili wasiweze kuona. Ipindishe migongo yao kwa mzigo wa matatizo.” Hivyo nauliza: Pale watu wa Mungu walipojikwaa na kuanguka, Je, hawakuweza kuinuka tena? Hakika hapana! Lakini kujikwaa kwao katika mwendo kulileta wokovu kwa wale wasio Wayahudi. Kusudi la hili lilikuwa kuwafanya Wayahudi wapate wivu. Kosa lao na hasara yao vilileta baraka za utajiri kwa ulimwengu kwa wasio Wayahudi. Hivyo fikirini ni kwa kiasi gani baraka hizi zitakuwa kubwa kwa ulimwengu pale idadi ya kutosha ya Wayahudi watakapokuwa watu wa aina ile anayoitaka Mungu. Nasema na ninyi watu msio Wayahudi. Kwa vile mimi ndiye ambaye Mungu ameniteua niwe mtume kwa wale wasio Wayahudi, nitafanya kwa bidii yote kuiheshimu huduma hii. Natarajia kuwafanya watu wangu wawe na wivu. Kwa njia hiyo, labda naweza kuwasaidia baadhi yao waweze kuokolewa. Mungu aliwaacha kwa muda. Hilo lilipotokea, akawa rafiki wa watu wengine ulimwenguni. Hivyo anapowakubali Wayahudi, ni sawa na kuwafufua watu baada ya kifo. Kama sehemu ya kwanza ya mkate inatolewa kwa Mungu, basi mkate mzima unakuwa umetakaswa. Kama mizizi ya mti ni mitakatifu, matawi ya mti huo pia ni matakatifu. Ni kama vile baadhi ya matawi ya mzeituni yamevunjwa, na tawi la mzeituni mwitu limeunganishwa katika ule mti wa kwanza. Ikiwa wewe si Myahudi, uko sawa na tawi la mzeituni mwitu, na sasa unashiriki nguvu na uhai wa mti wa kwanza. Lakini msienende kama mlio bora kuliko matawi yale yaliyovunjwa. Hamna sababu ya kujivuna, kwa sababu hamleti uhai katika mzizi. Mzizi ndiyo huleta uhai kwenu. Mnaweza kusema, “Matawi yalivunjwa ili niweze kuunganishwa katika mti wake.” Hiyo ni kweli. Lakini matawi hayo yalivunjwa kwa sababu hayakuamini. Na mnaendelea kuwa sehemu ya mti kwa sababu tu mnaamini. Msijivune, bali muwe na hofu. Ikiwa Mungu hakuyaacha matawi ya asili ya mti huo yawepo, hataweza kuwaacha ninyi muwepo mtakapoacha kuamini. Hivyo mnaona kwamba Mungu yu mwema, lakini anaweza pia kuwa mkali. Huwaadhibu wale wanaoacha kumfuata. Lakini ni mwema kwenu ikiwa mtaendelea kumwamini katika wema wake. Kama hamtaendelea kumtegemea yeye, mtakatwa kutoka katika mti. Na kama Wayahudi watamwamini Mungu tena, yeye atawapokea tena. Ana uwezo wa kuwarudisha pale walipokuwa. Kwa asili, tawi la mzabibu mwitu haliwezi kuwa sehemu ya mti mzuri. Lakini ninyi msio Wayahudi ni kama tawi lililovunjwa kutoka katika mzeituni pori. Na mliunganishwa na mti wa mzeituni ulio mzuri. Lakini Wayahudi ni kama matawi yaliyostawi kutokana na mti mzuri. Hivyo kwa hakika yanaweza kuunganishwa pamoja katika mti wao tena. Ndugu zangu, ieleweni siri hii ya ukweli. Kweli hii itawasaidia ninyi mjue kuwa hamfahamu kila kitu. Kweli ni hii: Sehemu ya Israeli wamefanywa kuwa wakaidi, lakini hiyo itabadilika wasio Wayahudi, wengi, watakapokuja kwa Mungu. Na hivyo ndivyo Israeli wote watakavyookolewa. Kama Maandiko yanavyosema, “Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; atauondoa uovu kutoka kwa wazaliwa wa Yakobo. Nami nitalifanya patano hili na watu wale nitakapoziondoa dhambi zao.” Kwa sasa, Wayahudi wanaokataa kuzipokea Habari Njema wamekuwa adui wa Habari Njema. Hili limetokea kwa manufaa yenu ninyi msio Wayahudi. Lakini bado Wayahudi ni wateule wa Mungu, na anawapenda kwa sababu ya ahadi alizozifanya kwa baba zao. Mungu habadili mawazo yake kuhusu watu anaowaita. Kamwe haamui kuzirudisha baraka alizokwisha kuwapa. Wakati mmoja ninyi pia mlikataa kumtii Mungu. Lakini sasa mmeipokea rehema, kwa sababu Wayahudi walikataa kutii. Na sasa wao ndiyo wanaokataa kutii, kwa sababu Mungu aliwaonesha ninyi rehema zake. Lakini hili limetokea ili nao pia waweze kupokea rehema kutoka kwake. Mungu amemfungia kila mmoja katika gereza la kutokutii. Lakini amefanya hivi ili aweze kuonesha rehema yake kwa wote. Ndiyo, utajiri wa Mungu ni mkuu sana! Hekima yake na ufahamu wake havina mwisho! Hakuna awezaye kuelezea yale Mungu anayoyaamua. Hayupo awezaye kuzielewa njia zake. Kama Maandiko yanavyosema, “Nani anaweza kuyajua yaliyo katika mawazo ya Bwana? Nani anaweza kumshauri?” “Nani amewahi kumpa Mungu kitu chochote? Mungu hadaiwi kitu chochote na mtu yeyote.” Ndiyo, Mungu ameviumba vitu vyote. Na kila kitu kinaendelea kuwepo kwa njia na kwa ajili yake. Utukufu uwe kwa Mungu milele yote! Amina. Hivyo, dada na kaka zangu, upokeeni wema mkuu ambao Mungu alituonyesha. Itoeni miili yenu kama sadaka hai kwake. Ishini kwa ajili ya Mungu tu na mweze kumpendeza yeye. Mkizingatia kwa makini yale aliyoyatenda, ni sahihi na inapasa kumwabudu Mungu kwa njia hii. Msifikiri au kuenenda kama watu wa ulimwengu huu, bali mruhusuni Mungu aibadilishe namna yenu ya kufikiri ndani yenu. Ndipo mtaweza kuelewa na kuyathibitisha yale Mungu anayotaka kutoka kwenu; yote yaliyo mema, yanayompendeza yeye na yaliyo makamilifu. Mungu amenipa mimi zawadi maalumu, na ndiyo sababu nina kitu cha kusema na kila mmoja wenu. Msifikiri kuwa ninyi ni bora kuliko jinsi mlivyo kwa asili. Mnapaswa kujiona kadri mlivyo. Mjipime wenyewe jinsi mlivyo kwa imani ambayo Mungu alimpa kila mmoja wetu. Kila mmoja wetu anao mwili mmoja, na mwili huo una viungo vingi. Viungo hivi vyote havifanyi mambo yanayofanana. Kwa jinsi hiyo hiyo, sisi ni watu wengi, lakini kwa sababu ni wa Kristo, sote ni mwili mmoja. Sisi sote ni viungo vya mwili huo, na kila kiungo ni sehemu ya viungo vingine vyote. Sote tunazo karama tofauti tofauti. Kila karama ilikuja kwa sababu ya neema aliyotupa Mungu. Yule aliye na karama ya unabii anapaswa kuitumia karama hiyo kwa namna inayokubalika kiimani. Aliye na karama ya kuhudumia anapaswa kuhudumia. Aliye na karama ya kufundisha anapaswa kufundisha. Aliye na karama ya kufariji wengine anapaswa kufanya hivyo. Aliye na karama ya kuhudumia mahitaji ya wengine anapaswa kutoa kwa moyo mweupe. Aliye na karama ya kuongoza anapaswa kufanya kwa juhudi katika hiyo. Aliye na karama ya kuonesha wema kwa wengine anapaswa kufanya hivyo kwa furaha. Upendo wenu unapaswa kuwa halisi. Uchukieni uovu. Fanyeni yaliyo mema tu. Pendaneni ninyi kwa ninyi kama wa familia moja. Na jitahidini kuwa wa kwanza katika kumpa heshima kila mmoja baina yenu. Mnapoendelea kumtumikia Bwana, fanyeni kwa juhudi wala msiwe wavivu. Mchangamke juu ya utumishi wenu kwa Mungu. Mfurahi kwa sababu ya tumaini mlilonalo. Mvumilieni mnapokutana na mateso. Ombeni nyakati zote. Washirikishe ulichonacho watu wa Mungu wanaohitaji msaada. Wakaribisheni katika nyumba zenu wale wanaosafiri au wanaohitaji msaada. Watakieni mema wale wanaowafanyia mabaya. Mwombeni Mungu awabariki, na sio kuwalaani. Furahini pamoja na wanaofurahi. Huzunikeni na wanaohuzunika. Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, lakini iweni radhi kuwa rafiki wa wasio na umuhimu kwa wengine. Msijihesabu kuwa wenye akili kuliko wengine wote. Mtu akikukosea, usimlipize ubaya. Mjaribu kufanya lile ambalo kila mtu anaona kuwa ni sahihi. Mjitahidi kadri mwezavyo kuishi kwa amani na kila mtu. Rafiki zangu, msijaribu kumwadhibu yeyote anayewakosea. Msubiri Mungu katika hasira yake awaadhibu. Katika Maandiko Bwana anasema, “Nitawaadhibu wao kwa ajili ya yale waliyofanya.” Badala yake, “ikiwa una adui wenye njaa, wapeni chakula wale. Ikiwa wana kiu, wapeni kinywaji wanywe. Kwa kufanya hivyo mtawafanya wajisikie aibu.” Msiruhusu uovu uwashinde, bali ushindeni uovu kwa kutenda mema. Watiini watawala wa serikali. Hakuna anayeweza kutawala bila mamlaka ya Mungu. Mamlaka ya kutawala hutoka kwa Mungu. Hivyo yeyote anayekuwa kinyume na serikali hakika anakuwa kinyume na kitu ambacho Mungu amekiweka. Wale walio kinyume na serikali wanajiletea adhabu wao wenyewe. Watu wanaotenda mema hawawaogopi watawala. Bali wale wanaotenda mabaya ni lazima wawaogope watawala. Je, mnataka kuwa huru mbali na kuwaogopa hao? Basi mfanye yaliyo sahihi tu, nao watawasifu ninyi. Watawala ni watumishi wa Mungu kwa ajili ya kuwasaidia ninyi. Lakini mkifanya yasiyo sahihi, mnayo sababu ya kuwa na woga. Hao wanayo mamlaka ya kuwaadhibu, na watayatumia mamlaka hayo. Wao ni watumishi wa Mungu ili wawaadhibu wale wanaofanya yale yasiyo sahihi. Kwa hiyo mnapaswa kuitii serikali, siyo tu kwa sababu mtaadhibiwa, bali kwa sababu mnajua kuwa ni jambo lililo sahihi kufanya hivyo. Na hii ndiyo sababu mnalipa kodi. Watawala hawa wanapaswa kulipwa kwa ajili ya kutimiza wajibu wao wote walionao wa kutawala. Hakika wanatumika kwa ajili ya Mungu. Wapeni watu wote vile wanavyowadai. Kama wanawadai aina yoyote ya kodi, basi lipeni. Onesheni heshima kwa wale mnaopaswa kuwaheshimu. Na onesheni uadilifu kwa wale mnaopaswa kuwafanyia hivyo. Msidaiwe chochote na mtu, isipokuwa mdaiwe upendo baina yenu. Mtu anayewapenda wengine anakuwa amefanya yote yanayoamriwa na sheria. Sheria inasema, “Usizini, usiue, usiibe, usitamani kitu cha mtu mwingine.” Amri hizo zote na zingine hakika zinajumlishwa na kuwa kanuni moja tu, “Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.” Upendo hauwaumizi wengine. Hivyo kupenda ni sawa na kuitii sheria yote. Nalisema hili kwa sababu mnajua kwamba tunaishi katika wakati ulio muhimu. Ndiyo, ni wakati wenu sasa kuamka kutoka usingizini. Wokovu wetu sasa uko karibu zaidi kuliko ilivyokuwa tulipoamini kwa mara ya kwanza. Usiku karibu umekwisha. Na mchana karibu unaingia. Hivyo tunapaswa kuacha kufanya chochote kinachohusiana na giza. Tunapaswa kujiandaa kuupiga uovu kwa silaha za nuru. Tunapaswa kuishi katika njia sahihi, kama watu walio wa mchana. Hatupaswi kuwa na tafrija za ovyo ama kulewa. Hatupaswi kujihusisha katika dhambi ya uzinzi au ya aina yoyote ya mwenendo usiofaa. Hatupaswi kusababisha mabishano au kuwa na wivu. Bali, muwe kama Kristo Yesu katika kila jambo mnalolitenda, ili watu watakapowaangalia, waweze kumwona yeye. Msifikirie namna ya kuridhisha matakwa ya udhaifu wa mwanadamu na tamaa zake. Iweni tayari kuwakubali wenye mashaka kuhusu yale ambayo waamini wanaweza kufanya. Tena msibishane nao kuhusu mawazo yao tofauti. Baadhi ya watu wanaamini kuwa wanaweza kula aina yoyote ya chakula, lakini wale walio na mashaka wanakula mboga za majani tu. Wale wanaojua kuwa wanaweza kula chakula cha aina yoyote hawapaswi kujisikia kuwa ni bora kuliko wale wanaokula mboga za majani tu. Na wale wanaokula mboga za majani tu hawapaswi kuamua kuwa wale wanaokula vyakula vyote wanakosea. Mungu amewakubali. Huwezi kuwahukumu watumishi wa mtu mwingine. Hilo linamhusu bwana wao mwenyewe ikiwa watafaulu au watashindwa. Na watakubaliwa, kwa sababu Bwana yuko tayari kuwafanya wafaulu. Watu wengine wanaweza kuamini kuwa siku moja ni ya muhimu zaidi kuliko nyingine. Na wengine wanaweza kuwa na uhakika kuwa siku zote ziko sawa. Kila mtu anapaswa kujihakikisha juu ya imani yake katika akili zake wenyewe. Wale wanaofikiri kuwa siku moja ni ya muhimu kuliko siku zingine wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Na wale wanaokula vyakula vya aina zote wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Ndiyo, wanamshukuru Mungu kwa ajili ya chakula. Na wale wanaokataa kula vyakula fulani wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Nao pia wanamshukuru Mungu. Hatuishi au kufa kwa ajili yetu sisi wenyewe tu. Kama tukiishi, tunaishi kwa ajili ya Bwana. Na kama tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Hivyo kuishi au kufa, sisi ni mali ya Bwana. Ndiyo sababu Kristo alikufa na kuishi tena ili awe Bwana juu ya wote waliokufa na wanaoishi. Hivyo kwa nini unamhukumu kaka au dada yako katika familia ya Mungu? Au kwa nini unafikiri kuwa wewe ni bora kuliko wao? Sote tutasimama mbele za Mungu, naye atatuhukumu sisi sote. Ndiyo, Maandiko yanasema, “‘Hakika kama niishivyo’, asema Bwana, ‘kila mtu atapiga magoti mbele zangu, na kila mtu atasema kuwa mimi ni Mungu.’” Hivyo kila mmoja wetu ataeleza kuhusu matendo yake mbele za Mungu. Hivyo tuache kuhukumiana sisi kwa sisi. Tuamue kutokufanya kitu ambacho kitasababisha matatizo kwa kaka au dada au kuathiri imani zao. Najua kuwa hakuna chakula ambacho kwa namna yake chenyewe hakifai kuliwa. Bwana Yesu ndiye aliyenithibitisha juu ya jambo hilo. Lakini ikiwa mtu ataamini kuwa si sahihi kula chakula fulani, basi kwake yeye huyo hiyo haitakuwa sahihi akila chakula hicho. Ikiwa utamuumiza kaka au dada yako kwa sababu ya chakula unachokula, hutakuwa unaifuata njia ya upendo. Kristo alikufa kwa ajili yao. Hivyo usiwaharibu kwa kula kitu wanachofikiri kuwa si sahihi kula. Usiruhusu kile ambacho ni chema kwako kiwe kitu watakachosema ni kiovu. Maisha katika ufalme wa Mungu siyo juu ya kile tunachokula na kunywa. Ufalme wa Mungu ni juu ya njia sahihi ya kuishi, amani na furaha. Vyote hii vinatoka kwa Roho Mtakatifu. Yeyote anayemtumikia Kristo kwa kuishi namna hii anampendeza Mungu na ataheshimiwa na wengine. Hivyo tujitahidi kwa kadri tuwezavyo kufanya kile kinacholeta amani. Tufanye kile kitakachomsaidia kila mtu kujengeka kiimani. Msiruhusu kula vyakula kuiharibu kazi ya Mungu. Vyakula vyote ni sahihi kula, lakini ni makosa kwa yeyote kula kitu kinachomletea shida kaka au dada katika familia ya Mungu. Ni heri kutokula nyama au kunywa divai au kufanya kitu chochote kinachoumiza imani ya kaka au dada yako. Ilindeni imani yenu kuhusu mambo haya kama siri kati yenu na Mungu. Ni baraka kufanya kile unachofikiri ni sahihi bila kujihukumu mwenyewe. Lakini ikiwa unakula kitu bila kuwa na uhakika kuwa ni sahihi, unakosea. Hii ni kwa sababu hukuamini kuwa ni sahihi. Na ukifanya chochote unachoamini kuwa si sahihi, hiyo ni dhambi. Baadhi yetu hatuna matatizo na mambo haya. Hivyo tunapaswa kuwa wastahimilivu kwa wale wasio imara na wenye mashaka. Hatupaswi kufanya yanayotupendeza sisi bali tufanye yale yanayowapendeza wao na kwa faida yao. Tufanye chochote kinachoweza kumsaidia kila mtu kujengeka katika imani. Hata Kristo hakuishi ili kijaribu kujifurahisha yeye mwenyewe. Kama Maandiko yanavyosema, “Matusi ambayo watu waliyatoa dhidi yako pia yalinifanya niteseke.” Chochote kilichoandikwa zamani kiliandikwa ili kitufundishe sisi. Maandiko haya yaliandikwa ili yatupe matumaini yanayokuja kwa njia ya subira na kutia moyo kunakoletwa nayo. Subira na kuhimiza kote hutoka kwa Mungu. Na ninawaombea ili Mungu awasaidie muwe na nia ile ile ninyi kwa ninyi, kama ilivyo nia ya Kristo Yesu. Kisha ninyi nyote, kwa sauti moja, mtamtukuza Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kristo aliwakaribisha ninyi, hivyo nanyi mkaribishane ninyi kwa ninyi. Hili litaleta heshima kwa Mungu. Ndiyo, haya ndiyo maneno yangu kwenu kwamba Kristo alifanyika mtumishi wa Wayahudi ili kuonesha kuwa Mungu amefanya yale aliyowaahidi baba zao wakuu. Na pia alifanya hivi ili wale wasio Wayahudi waweze kumsifu Mungu kwa rehema anazowapa. Maandiko yanasema, “Hivyo nitakushukuru wewe katikati ya watu wa mataifa mengine; Nitaliimbia sifa jina lako.” Na Maandiko yanasema, “Ninyi watu wa mataifa mengine furahini pamoja na watu wa Mungu.” Pia Maandiko yanasema, “Msifuni Bwana ninyi watu wote wa mataifa mengine; watu wote na wamsifu Bwana.” Na Isaya anasema, “Mtu mmoja atakuja kutoka katika ukoo wa Yese. Atainuka na kutawala juu ya mataifa, na wataweka matumaini yao kwake.” Naomba kwamba Mungu aletaye matumaini awajaze furaha na amani kadri mnavyomwamini yeye. Na hii isababishe tumaini lenu liongezeke hadi lifurike kabisa ndani yenu kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Kaka na dada zangu, najua pasipo mashaka kuwa mmejaa wema na mnayo maarifa yote mnayohitaji. Hivyo kwa hakika mnaweza kushauriana ninyi kwa ninyi. Lakini nimewaandikia ninyi kwa ujasiri wote kuhusu mambo fulani niliyotaka mkumbuke. Nilifanya hivi kwa sababu Mungu alinipa karama hii maalumu: kuwa mtumishi wa Kristo Yesu kwa ajili ya wasio Wayahudi. Natumika kama kuhani ambaye kazi yake ni kuhubiri Habari Njema kutoka kwa Mungu. Alinipa mimi jukumu hili ili ninyi msio Wayahudi mweze kuwa sadaka atakayoikubali, sadaka iliyotakaswa na Roho Mtakatifu. Na hii ndiyo sababu najisikia vizuri kuhusu yale yote yaliyofanyika kwa ajili ya Mungu kwa kuwa mimi ni mali ya Kristo Yesu. Sitazungumzia chochote nilichofanya mwenyewe. Nitazungumza tu kuhusu yale Kristo aliyofanya akinitumia mimi katika kuwaongoza wale wasiokuwa Wayahudi katika kutii. Ni yeye aliyetenda kazi katika yale niliyosema na kufanya. Alitenda kazi kwa ishara za miujiza kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Matokeo yake ni kuwa nimewahubiri watu Habari Njema kuhusu Kristo kuanzia Yerusalemu na kuzunguka kote mpaka Iliriko. Na hivyo nimemaliza sehemu hiyo ya wajibu wangu. Imekuwa shabaha yangu daima kuzihubiri Habari Njema katika sehemu ambako watu hawajawahi kusikia juu ya Kristo. Nafanya hivi kwa sababu sitaki kujenga katika kazi ambayo tayari mtu mwingine amekwisha kuianza. Kama Maandiko yanavyosema, “Wale ambao hawakuambiwa kuhusu yeye wataona, na wale ambao hawajasikia juu yake wataelewa.” Kazi hiyo imenifanya niwe na shughuli nyingi sana na mara nyingi imenizuia kuja kuwaona. Kwa miaka mingi nimetamani kuwatembelea, na sasa nimekamilisha kazi yangu katika maeneo haya. Hivyo nitawatembelea nitakapoenda Hispania. Ndiyo, napanga kusafiri kwenda Hispania na natumaini kuwatembelea nikiwa njiani. Nitakaa kwa muda na kufurahi pamoja nanyi. Kisha natumaini mtanisaidia kuendelea na safari yangu. Sasa ninakwenda Yerusalemu kuwasaidia watu wa Mungu huko. Baadhi yao ni maskini, na waamini kule Makedonia na Akaya walitaka kuwasaidia. Hivyo walikusanya kiasi cha fedha ili wawatumie. Walifurahia kufanya hivi. Na ilikuwa kama kulipa kitu fulani walichokuwa wakidaiwa, kwa sababu kama watu wasiokuwa Wayahudi walikuwa wamebarikiwa kiroho na Wayahudi. Hivyo nao wanapaswa kutumia baraka za vitu walivyonavyo kwa ajili ya kuwasaidia Wayahudi. Naelekea Yerusalemu kuhakikisha kuwa maskini wanapokea fedha hizi zilizotolewa kwa ajili yao. Nitakapokuwa nimekamilisha hilo, nitaondoka kuelekea Hispania na nikiwa njiani nitasimama ili niwaone. Na ninajua kwamba nitakapowatembelea, nitakuja na baraka zote anazotoa Kristo. Kaka na dada zangu, nawaomba mnisaidie katika kazi hii kwa kuniombea kwa Mungu. Fanyeni hivi kwa sababu ya Bwana wetu Yesu Kristo na pendo ambalo Roho anatupa. Niombeeni ili niokolewe kutokana na wale walioko Yudea wanaokataa kuupokea ujumbe wetu. Pia ombeni kwamba msaada huu ninaoupeleka Yerusalemu utakubalika kwa watu wa Mungu huko. Kisha, nitakuwa na furaha wakati nitakapokuja kuwaona, Mungu akipenda. Na ndipo tutaweza kufurahia muda wa kujengana sisi kwa sisi. Mungu anayetoa amani awe pamoja nanyi nyote. Amina. Napenda mjue kuwa mnaweza kumwamini dada yetu Foebe. Ni mtumishi maalum wa kanisa la kule Kenkrea. Nawaomba mmkaribishe kama yule aliye wa Bwana. Mkaribisheni kwa jinsi ambayo watu wa Mungu wanapaswa. Msaidieni kwa chochote atakachohitaji kutoka kwenu. Yeye amekuwa kiongozi anayeheshimika ambaye amewasaidia watu wengine wengi, pamoja na mimi. Mpeni salamu Priska na Akila, ambao wametumika pamoja nami kwa ajili ya Kristo Yesu. Waliyahatarisha maisha yao wenyewe ili wayaokoe maisha yangu. Nawashukuru hao, na makanisa yote ya wasio Wayahudi yanawashukuru wao. Vilevile, fikisheni salamu katika kanisa linalokusanyikia nyumbani mwao. Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto. Alikuwa mtu wa kwanza kumfuata Kristo kule Asia. Pia msalimieni Mariamu ambaye alifanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili yenu. Pia msalimieni Androniko na Yunia. Hao ni jamaa zangu, na walikuwa gerezani pamoja nami. Walikuwa wafuasi wa Kristo kabla yangu. Nao ni miongoni mwa wale walio muhimu sana waliotumwa na Kristo kuifanya kazi yake. Msalimuni Ampliato, rafiki yangu mpendwa miongoni mwa watu wa Bwana, na kwa Urbano. Aliyefanya kazi pamoja nasi kwa ajili ya Kristo. Pia fikisheni salamu kwa rafiki yangu mpendwa Stakisi na Apele, aliyejithibitisha kuwa yeye ni mfuasi wa kweli wa Kristo. Nisalimieni watu wote katika nyumba ya Aristobulo na Herodioni, jamaa yangu. Wasalimieni nyumba nzima ya Narkiso aliye wake Bwana na Trifaina na Trifosa, wanawake wanaofanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili ya Bwana. Nisalimieni rafiki yangu mpendwa Persisi. Dada huyu amefanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili ya Bwana. Pia msalimieni Rufo, mmoja wa wateule wa Bwana, na mama yake, ambaye amefanyika mama yangu pia. Fikisheni salamu kwa Asinkrito, Flegoni, Hermesi, Patroba, Herma na waamini wote walio pamoja nao. Msalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, Olimpa na watu wote wa Mungu walio pamoja nao. Mpeni kila mmoja ile salamu maalum ya watu wa Mungu. Makanisa yote yaliyo ya Kristo yanatuma salamu zao kwenu. Kaka na dada zangu, ninataka muwe macho na wale wanaosababisha mabishano na kuumiza imani za watu kwa kufundisha mambo ambayo ni kinyume cha yale mliyojifunza. Mjitenge nao. Watu wa namna hiyo hawamtumikii Kristo Bwana wetu. Wanajifurahisha wenyewe tu. Wanatumia mazungumzo matamu na kusema mambo yanayopendeza ili kuwadanganya wale wasiojua kuhusu uovu. Kila mtu amesikia juu ya utii wenu kwa Bwana, nami nafurahi sana juu ya hilo. Lakini ninataka muwe werevu kuhusu yaliyo mema na kutokujua lolote kuhusu yaliyo maovu. Mungu mwenye kuleta amani atamwangamiza Shetani mapema na kuwapa nguvu juu yake. Neema ya Bwana wetu Yesu iwe pamoja nanyi. Timotheo, mtumishi pamoja nami, anawatumieni salamu. Pia Lukio, Yasoni na Sosipatro (hawa ni jamaa zangu) wanawatumieni salamu. Mimi Tertio, ninayeandika barua hii kwa ajili ya Paulo. Ninawasalimu kama mmoja aliye wa Bwana. Gayo ameniruhusu na kanisa lote hapa kuitumia nyumba yake. Anawatumia salamu zake. Erasto na kaka yetu Kwarto pia wanatuma salamu. Erasto ndiye mtunza hazina wa mji hapa. *** Atukuzwe Mungu! Yeye ndiye anayeweza kuzitumia Habari Njema ninazozifundisha kuwaimarisha katika imani. Ni ujumbe ninaowaambia watu kuhusu Yesu Kristo. Ujumbe huo ni siri ya ukweli iliyofichwa kwa karne nyingi sana lakini sasa imefunuliwa. Na kweli hiyo sasa imeonyeshwa kwetu. Ilijulishwa kwa yale ambayo manabii waliandika katika Maandiko, kama Mungu wa milele alivyoagiza. Na sasa imejulikana kwa mataifa yote ili waweze kuamini na kumtii yeye. Utukufu wa milele ni kwa Mungu mwenye hekima pekee kwa njia ya Yesu Kristo. Amina. Salamu kutoka kwa Paulo. Mimi ni mtume kwa sababu Kristo Yesu alinichagua. Alinichagua kwa sababu hivyo ndivyo Mungu alitaka. Naandika barua hii kwa msaada wa Sosthenesi aliye kaka yetu katika Kristo. Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, ninyi ambao mmefanywa watakatifu kwa sababu mmeunganishwa kwa Kristo Yesu. Mlichaguliwa kuwa watakatifu wa Mungu pamoja na watu wote kila mahali wanaomwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wao na Bwana wetu. Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi. Ninamshukuru Mungu daima kwa sababu ya neema aliyowapa katika Kristo Yesu. Ambaye kwa njia yake Mungu amewabariki sana kwa namna mbalimbali hata miongoni mwenu wapo watu wenye vipawa vya kuzungumza na wengine wana vipawa vya maarifa! Hii ni kwa sababu yale tuliyowaambia kuhusu Kristo yamedhihirika kuwa kweli katikati yenu. Na sasa mna karama zote mnapomsubiri Mungu audhihirishie ulimwengu jinsi Bwana wetu Yesu Kristo alivyo wa ajabu. Ataendelea kuwatia nguvu na hakuna atakayeweza kuwashtaki mpaka siku ya mwisho Bwana wetu Yesu atakaporudi. Mungu ni mwaminifu. Na ndiye aliyewachagua ninyi ili mshiriki uzima pamoja na Mwanaye, Yesu Kristo Bwana wetu. Ndugu zangu, kwa mamlaka ya Bwana wetu Yesu Kristo, ninawasihi mpatane ninyi kwa ninyi. Msigawanyike katika makundi. Lakini iweni pamoja tena katika kuwaza kwenu na katika nia zenu. Kaka na dada zangu, baadhi ya jamaa wa Kloe wamenitaarifu kuwa kuna mabishano miongoni mwenu. Baadhi yenu husema, “Mimi ninamfuata Paulo,” na mwingine husema, “Mimi ninamfuata Apolo.” Mwingine husema, “Mimi ninamfuata Petro,” na mwingine husema, “Mimi ninamfuata Kristo.” Kristo hawezi kugawanywa katika makundi. Je, Paulo ndiye alikufa msalabani kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa katika jina la Paulo? Ninashukuru kwa kuwa sikumbatiza mtu yeyote kwenu isipokuwa Krispo na Gayo. Ninashukuru kwa sababu hakuna anayeweza kusema kuwa mlibatizwa katika jina langu. (Niliwabatiza pia watu wote wa nyumbani mwa Stefana, lakini sikumbuki kuwa niliwabatiza watu wengine) Kristo hakunipa kazi ya kubatiza watu. Alinipa kazi ya kuhubiri Habari Njema pasipo kutumia hekima ya maneno, inayoweza kubatilisha nguvu iliyo katika msalaba wa Kristo. Mafundisho kuhusu msalaba yanaonekana ni ya kipuuzi kwao wao wanaoelekea kwenye uharibifu. Lakini ni nguvu ya Mungu kwetu sisi tunaookolewa. Kama Maandiko yanavyosema, “Nitaiharibu hekima ya wenye hekima. Nitaukanganya uelewa wa wenye akili.” Je, hii inasema nini kuhusu mwenye hekima, mtaalamu wa sheria au yeyote katika ulimwengu huu mwenye ujuzi wa kutengeneza hoja zenye nguvu? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upuuzi. Hii inadhihirisha wazi kuwa, Mungu katika hekima yake aliamua kuwa hawezi kupatikana kwa kutumia hekima ya ulimwengu. Hivyo Mungu aliutumia ujumbe unaoonekana kuwa upuuzi kuwaokoa wale wanaouamini. Na hii ndiyo sababu Wayahudi wanataka ishara za miujiza na Wayunani wanataka hekima. Lakini ujumbe tunaomwambia kila mtu unahusu Masihi aliyekufa msalabani. Ujumbe huu ni kikwazo kwa Wayahudi na kwa Wayunani ni upuuzi. Lakini kwa Wayahudi na Wayunani walioteuliwa na Mungu, Masihi huyu aliyesulibiwa ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Maana upumbavu wa Mungu ni hekima zaidi ya hekima ya kibinadamu, na udhaifu wa Mungu ni nguvu zaidi ya nguvu ya kibinadamu. Kaka na dada zangu, fikirini kuhusu hili kwamba Mungu aliwachagua ili muwe milki yake. Wachache wenu mlikuwa na hekima kwa namna dunia inavyoichukulia hekima. Wachache wenu mlikuwa mashuhuri na wachache wenu mnatoka katika familia maarufu. Lakini Mungu aliyachagua mambo ambayo wanadamu huyachukulia kuwa ya kipumbavu ili ayaaibishe yenye hekima. Aliyachagua mambo yanayoonekana kuwa manyonge ili ayaaibishe yenye nguvu. Aliwachagua wasio kitu ili ayaangamize yale ambayo ulimwengu unadhani ni muhimu. Mungu alifanya hivi ili mtu yeyote asisimame mbele zake na akajisifu kuwa yeye ni bora kuliko mwingine. Lakini Mungu ameyafungamanisha maisha yenu na Kristo Yesu. Yeye alifanywa kuwa hekima yetu kutoka kwa Mungu. Na kupitia kwake tumehesabiwa haki na Mungu na tumefanywa kuwa watakatifu. Kristo ndiye aliyetuokoa, akatufanya watakatifu na akatuweka huru mbali na dhambi. Hivyo, kama Maandiko yanavyosema, “Kila anayejisifu, ajisifu juu ya Bwana tu.” Wapendwa kaka na dada zangu katika Kristo, nilipokuja kwenu, niliwaambia siri ya kweli iliyofunuliwa na Mungu. Lakini sikuja kama mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuongea au mwenye hekima ya juu. Nilipokuwa pamoja nanyi, niliamua kusahau kila kitu isipokuwa Yesu Kristo na kifo chake msalabani. Nilipokuja kwenu nilikuwa mdhaifu na mwenye hofu. Mafundisho na kuzungumza kwangu hakukuwa kwa maneno yenye hila. Lakini uthibitisho wa mafundisho yangu ilikuwa nguvu inayotolewa na Roho. Nilifanya hivi ili imani yenu iwe katika nguvu ya Mungu siyo katika hekima ya kibinadamu. Tunafundisha hekima kwa watu ambao macho yao yamefunguliwa ili waione hekima ya siri ya Mungu. Si hekima ya watawala wa ulimwengu huu wanaobatilika. Tunaisema hekima ya Mungu katika namna ambayo baadhi wanaweza kuiona na wengine hawawezi. Ni hekima iliyofichwa mpaka wakati huu na Mungu aliipanga hekima hii kabla ya kuumba ulimwengu, kwa ajili ya utukufu wetu. Hakuna mtawala yeyote wa ulimwengu huu aliyeielewa hekima hii. Ikiwa wangeielewa, wasingemwua Bwana wetu mkuu na mwenye utukufu mwingi msalabani. Lakini kama Maandiko yanavyosema, “Hakuna aliyewahi kuona, hakuna aliyewahi kusikia, hakuna aliyewahi kufikiri kuhusu kile ambacho Mungu amewaandalia wanaompenda.” Lakini Mungu ametuonesha mambo haya kupitia Roho. Roho anaweza kuchunguza mambo yote. Anajua hata siri za ndani kabisa za Mungu. Hakuna mtu anayejua mawazo ya mtu mwingine. Ni roho inayoishi ndani ya mtu huyo ndiyo inajua mawazo ya mtu huyo. Ndivyo ilivyo hata kwa Mungu, ni Roho wa Mungu peke yake ndiye anayeyajua mawazo ya Mungu. Tulipokea Roho wa Mungu, si roho wa ulimwengu. Tulimpokea Roho wa Mungu ili tuweze kujua yote aliyotupa Mungu. Tunapozungumza, hatutumii hoja tulizofundishwa na wenye hekima. Bali hoja tulizofundishwa na Roho. Tunatumia hoja za Roho kuelezea kweli za Roho. Watu wasio na Roho wa Mungu, hawakubali vitu vinavyotoka kwa Roho. Hudhani kuwa ni vitu vya kipuuzi. Hawavielewi, kwa sababu havieleweki pasipo msaada wa Roho. Aliye na Roho anaweza kujua mambo yote anayofundisha Roho. Na hatutahukumiwa kuwa na hatia na mtu yeyote. Kama Maandiko yanavyosema, “Nani anaweza kujua anachokiwaza Bwana? Nani anaweza kumshauri?” Lakini sisi tumepewa tunawaza kama Kristo. Ndugu zangu, nilipokuwa kwenu, sikuzungumza nanyi kama ninavyozungumza na watu wanaoongozwa na Roho. Nilizungumza nanyi kama watu wa kawaida wa duniani. Mlikuwa kama watoto katika Kristo. Mafundisho niliyowafundisha yalikuwa kama maziwa, siyo chakula kigumu. Nilifanya hivi kwa kuwa hamkuwa tayari kwa chakula kigumu. Na hata sasa hamjawa tayari. Bado hamwenendi katika Roho, mnaoneana wivu na mnabishana ninyi kwa ninyi kila wakati. Hii inaonesha kuwa bado mnazifuata tamaa zenu wenyewe. Mnaenenda kama watu wa kawaida wa ulimwengu huu. Mmoja wenu anasema, “Mimi ninamfuata Paulo,” na mwingine anasema, “Ninamfuata Apolo.” Mnaposema mambo kama haya, mnaenenda kama watu wa ulimwengu. Je, Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Apolo na mimi si watumishi tu ambao Mungu alitutumia ili mmwamini Yesu Kristo. Kila mmoja wetu alifanya kazi aliyopewa na Bwana. Nilipanda mbegu na Apolo akamwagilia maji. Lakini Mungu ndiye aliyeiotesha na kuikuza. Hivyo aliyepanda na kuimwagilia si wa muhimu. Mungu ndiye wa muhimu, kwa sababu ndiye anayevifanya vitu viote vikue. Anayepanda na anayemwagilia maji wote wana nia moja. Na kila mmoja atalipwa kutokana na kazi yake yeye mwenyewe. Ninyi ni shamba la Mungu, ambamo tulifanya kazi pamoja kwa ajili yake. Nanyi pia ni jengo la Mungu. Nami kama mjenzi stadi nilijenga msingi wa nyumba hiyo kwa kutumia karama alizonipa Mungu. Wengine wanajenga pia katika msingi huo. Lakini kila mtu lazima awe mwangalifu kwa namna anavyojenga. Yesu Kristo ndiye msingi uliokwishajengwa, na hakuna yeyote anayeweza kujenga msingi mwingine. Watu wanaweza kujenga juu ya msingi huo kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, mbao, nyasi au majani. Kila kazi atakayoifanya kila mtu itaonekana siku ya hukumu itakapofika, na itaonekana ilivyo mbaya au nzuri. Siku hiyo kila kazi ya mtu itajaribiwa kwa moto. Mungu atampa thawabu mtu anayejenga juu ya msingi huu ikiwa kazi yake haitateketea kwa moto. Lakini ikiwa itateketea atapata hasara. Lakini yeye mwenyewe ataokolewa, lakini itakuwa kama mtu anayeokolewa kutoka kwenye moto. Hakika mnajua kuwa ninyi ni hekalu la Mungu na Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Ndiyo, ninyi nyote kwa pamoja ni Hekalu la Mungu. Na yeyote atakayeliharibu Hekalu la Mungu ataadhibiwa na Mungu, kwa sababu Hekalu la Mungu ni mali yake yeye mwenyewe. Msijidanganye. Yeyote anayejiona kuwa ana hekima kwa viwango vya ulimwengu huu, basi na awe mpumbavu. Hiyo ndiyo njia pekee itakayomfanya kuwa na hekima. Ninasema hivi kwa sababu hekima ya ulimwengu huu ni upumbavu kwa Mungu. Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu huwanasa katika mitego yao wenyewe wale wanaojidhania kuwa na hekima.” Pia Maandiko yanasema, “Bwana anajua mawazo ya wenye hekima. Anajua kuwa mawazo yao hayana maana.” Hivyo hakuna mtu yeyote duniani ambaye ninyi mnapaswa kujivunia. Kila kitu ni chenu: Paulo, Apolo, Petro, ulimwengu, uzima, mauti, wakati uliopo na ujao, vyote hivi ni vyenu. Ninyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu. Tuchukulieni sisi kuwa ni watumishi wa Kristo, ambao Mungu ametuamini tufanye kazi ya kuwaambia wengine siri zake za kweli. Wale walioaminiwa kwa kazi muhimu kama hii imewapasa kuonesha ya kuwa wao ni waaminifu. Lakini siichukulii hukumu yenu kuhusu hili kuwa kitu. Hata hukumu yo yote katika mahakama ya kibinadamu isingekuwa na maana yoyote. Sijihukumu hata mimi mwenyewe. Sikumbuki kosa lolote nililofanya, lakini hiyo hainifanyi mimi kujihesabia haki. Bwana pekee ndiye anayepaswa kunihukumu ikiwa nimefanya vyema au la. Hivyo, msimhukumu mtu yeyote sasa. Hukumu itakuwa wakati Bwana atakaporudi. Ataangaza mwanga kwa kila kitu kilichofichwa gizani. Ataziweka wazi nia za siri za mioyo yetu. Ndipo sifa ambayo kila mtu anapaswa kuipata itatoka kwa Mungu. Ndugu zangu, nimemtumia Apolo na mimi mwenyewe kama mfano kwa ajili yenu. Nimefanya hivi ili mjifunze kutoka kwetu maana ya maneno yanayosema, “Uwe mwangalifu kufuata kilichoandikwa.” Kwa nini mnajisifu? Mlipewa kila kitu mlicho nacho. Sasa, ikiwa mlipewa kila kitu mlicho nacho, kwa nini mnajisifu kana kwamba mlipata vitu vyote kwa nguvu zenu wenyewe? Mnadhani kwamba tayari mna kila kitu mnachohitaji. Mnadhani kwamba mmekwisha tajirika. Laiti mngekwisha fanywa wafalme, kwa sababu tungekuwa wafalme pamoja nanyi. Lakini inaonekana kana kwamba Mungu amenipa mimi na mitume wengine mahali pa mwisho. Sisi ni kama wafungwa waliohukumiwa kufa, waliosimamishwa katika gwaride ili ulimwengu wote uwaone, si watu tu bali hata malaika pia. Tu wapumbavu kwa kuwa sisi ni wa Kristo, lakini mnadhani kuwa ninyi ni wenye hekima katika Kristo. Sisi ni dhaifu, lakini mnadhani kuwa mna nguvu. Watu wanawaheshimu ninyi, na hawatuheshimu sisi. Hata sasa hatuna vyakula vya kutosha kula au kunywa, na hatuna nguo za kutosha. Mara kwa mara tunapigwa na hatuna makazi. Tunafanya kazi sana kwa mikono yetu ili tupate chakula. Watu wanapotutukana, tunamwomba Mungu awabariki. Watu wanapotutendea vibaya, tunavumilia. Watu wanaposema mabaya juu yetu, tunawajibu kwa upole. Lakini watu wanaendelea kutuona kama takataka. Siwaambii haya ili kuwatahayarisha, lakini ninaandika haya ili kuwaonya kama watoto wangu mwenyewe ninaowapenda. Mnaweza kuwa na walimu elfu kumi katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Kupitia Habari Njema mimi nilifanyika baba kwenu katika Kristo Yesu. Ndiyo sababu ninawahimiza mfuate mfano wangu. Ndiyo sababu ninamtuma Timotheo kwenu. Ni mwanangu katika Bwana. Ninampenda na ni mwaminifu. Atawasaidia ili mkumbuke namna ninavyoishi kama mfuasi wa Kristo Yesu, kama ninavyofundisha katika kila kanisa kila mahali ninakokuwa. Baadhi yenu mnajivuna, mkidhani kuwa sitakuja kuwatembelea tena. Lakini nitakuja kwenu hivi karibuni ikiwa Bwana atanijalia. Ndipo nitajua ikiwa hawa wanaojivuna wana nguvu za kutenda jambo lolote zaidi ya kuzungumza. Mungu huonesha kuwa anatawala katika maisha kwa yale wanayoweza kufanya na si kwa maneno yao. Je, nitakapokuja kwenu, nije nikiwa na adhabu au nije kwa upendo na upole? Sitaki kuyaamini yale ninayosikia, ya kwamba kuna uzinzi katikati yenu. Na ni aina mbaya ya uzinzi ambayo hata wasiomwamini Mungu wetu hawauruhusu. Watu wanasema kuwa huko kwenu kuna mtu anayetenda dhambi ya zinaa na mke wa baba yake. Na mna kiburi! Mngepaswa kuwa na huzuni badala yake. Na mtu aliyetenda dhambi hiyo ilipaswa kuwa amefukuzwa kutoka katika kundi lenu. Siwezi kuwa hapo pamoja nanyi ana kwa ana, lakini niko pamoja nanyi katika roho. Na nimekwisha mhukumu mtu aliyetenda hii kama ambavyo ningemhukumu ikiwa ningekuwa hapo. Nanyi pia mnapaswa kufanya vivyo hivyo. Kusanyikeni pamoja katika jina la Bwana wetu Yesu. Nitakuwa pamoja nanyi katika roho, na nguvu ya Bwana Yesu itakuwa pamoja nanyi. Mtoeni mtu huyu kwa Shetani ili tabia yake ya kujisifu iangamizwe lakini mtu mwenyewe na kanisa, lilojazwa Roho, liweze kuokolewa siku Bwana atakaporudi. Kujisifu kwenu si kuzuri. Mnajua msemo unaosema, “Chachu kidogo huchahua donge zima.” Ondoeni chachu ya zamani ili muwe donge jipya. Ninyi kwa hakika ni mkate usio na chachu, mkate wa Pasaka, Ndiyo, Kristo aliye Mwanakondoo wetu wa Pasaka amekwisha usawa. Hivyo na tuule mlo wetu wa Pasaka, lakini si pamoja na mkate wenye chachu ya zamani, yaani dhambi na matendo mabaya. Lakini tule mkate usio na chachu. Huu ni mkate wenye ukweli na chachu njema. Katika barua yangu niliwaandikia kuwa msishirikiane na wazinzi. Lakini sikuwa na maana ya watu wa ulimwengu huu. La sivyo ingewalazimu kuhama katika ulimwengu huu ili mweze kujitenga na wazinzi au walio walafi na waongo, au wale wanaoabudu sanamu. Nilikuwa na maana kuwa msishirikiane na mtu yeyote yule anayedai kuwa anaamini lakini anaendelea kuishi katika dhambi. Usimkaribishe nyumbani kwa chakula kaka ama dada aliye mzinzi, mlafi, anayeabudu sanamu, mtukanaji, mlevi au mwongo. Si kazi yangu kuwahukumu wasio sehemu ya kundi la waamini. Mungu atawahukumu, lakini ni lazima mwahukumu wale walio katika kundi lenu. Maandiko yanasema, “Mwondoe mwovu katika kundi lako.” Kwa nini mnakwenda kwenye mahakama za kisheria mmoja wenu anapokuwa na shauri dhidi ya mwingine aliye miongoni mwenu? Mnajua ya kwamba mahakimu wa aina hiyo hawawezi kutegemewa kuamua kwa haki iliyo ya kweli. Sasa kwa nini mnawaruhusu wawaamulie aliye na haki? Kwa nini msiwaruhusu watakatifu wa Mungu waamue ni nani aliye na haki? Hamjui kuwa watakatifu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Hivyo, ikiwa mtauhukumu ulimwengu, hakika mnaweza kutatua mashauri kama hayo miongoni mwenu. Hakika mnajua kuwa tutawahukumu malaika. Kwa kuwa hiyo ni kweli basi hakika tunaweza kuhukumu masuala ya kawaida ya maisha. Sasa, ikiwa mna masuala kama haya ya kawaida ya maisha yanayotakiwa kuamuliwa, kwa nini mnayapeleka kwa wasio waamini? Hao ambao hawana umuhimu wo wote kwenu? Ninasema hivi ili kuwatahayarisha. Nina uhakika yupo mwenye hekima miongoni mwa waamini katika kanisa lenu anayeweza kutatua mgogoro kati ya waamini wawili. Lakini sasa mwamini mmoja anamshtaki mwamini mwenzake na mnaruhusu watu wasio waamini wawaamulie! Ule ukweli kuwa mnayo mashitaka baina yenu ninyi kwa ninyi tayari ni uthibitisho wa kushindwa kwenu kabisa. Ingekuwa bora kwenu kustahimili yasiyo haki ama kulaghaiwa. Lakini ninyi ndiyo mnaotenda mabaya kwa kudanganya. Na mnawafanyia hivi ndugu zenu katika Kristo! Msijidanganye. Hamjui ya kuwa wanaowatendea mabaya hawana nafasi katika ufalme wa Mungu. Ninasema kuhusu wazinzi, wanaoamini miungu wa uongo, wasio waaminifu katika ndoa, nao wanaolawitiana. Pia wezi, walafi, walevi, watukanaji, au waongo wanaowadanganya wengine ili wawaibie hawatakuwa na sehemu katika ufalme wa Mungu. Baadhi yenu mlikuwa hivyo huko nyuma. Lakini mlisafishwa mkawa safi, mkafanywa kuwa watakatifu na mkahesabiwa haki na Mungu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu. Mtu mmoja anaweza kusema, “Ninaruhusiwa kufanya kitu chochote.” Nami ninawaambia ya kuwa si vitu vyote vilivyo na manufaa. Hata kama ni kweli kuwa “Ninaruhusiwa kufanya kitu chochote,” Sitaruhusu kitu chochote kinitawale kama vile ni mtumwa. Mmoja wenu anasema, “Chakula ni kwa ajili ya tumbo na tumbo ni kwa ajili ya chakula, na Mungu ataviteketeza vyote.” Hiyo ni dhahiri, lakini mwili si kwa ajili ya zinaa, bali kwa ajili ya Bwana, na Bwana ni kwa ajili ya mwili. Na Mungu ataifufua pia miili yetu kutoka kwa wafu kwa nguvu yake, kama alivyomfufua Bwana Yesu. Hakika mnajua kuwa miili yenu ni sehemu ya Kristo mwenyewe. Hivyo sitakiwi kamwe kuchukua sehemu ya Kristo na kuiunganisha na kahaba! Maandiko yanasema, “Watu wawili watakuwa mmoja.” Hivyo mnapaswa kujua kuwa kila aliyeungana na kahaba, amekuwa mwili mmoja na kahaba. Lakini aliyeungana na Bwana, yu mmoja naye katika roho. Hivyo ikimbieni dhambi ya uzinzi. Mnasema kuwa, “Kila dhambi ni kitu kilichomo katika akili tu haihusiki na mwili.” Lakini ninawaambia, anayetenda dhambi ya uzinzi anautendea dhambi mwili wake mwenyewe. Nina uhakika mnajua kuwa mwili wenu ni hekalu kwa ajili ya Roho Mtakatifu mliyepewa na Mungu na Roho Mtakatifu anaishi ndani yenu. Hamjimiliki ninyi wenyewe. Mungu alilipa gharama kubwa ili awamiliki. Hivyo mtukuzeni Yeye kwa kutumia miili yenu. Sasa nitazungumza kuhusu mambo yale mliyoniandikia. Mliuliza ikiwa ni bora mwanaume asimguse mwanamke kabisa. Lakini dhambi ya uzinzi ni ya hatari, hivyo kila mwanaume anapaswa kumfurahia mke wake, na kila mwanamke anapaswa kumfurahia mume wake. Mume anapaswa kumtosheleza mkewe, vivyo hivyo mke amtosheleze mume wake. Mke hana mamlaka kabisa juu ya mwili wake, bali mume ana mamlaka juu ya mwili wa mkewe. Mume hana mamlaka kabisa juu ya mwili wake, bali mke ana mamlaka juu ya mwili wa mumewe. Msinyimane miili yenu. Lakini mnaweza kukubaliana kutojamiiana kwa muda ili mtumie muda huo katika maombi. Kisha mkutane tena ili Shetani asiwajaribu kutokana na kushindwa kujizuia tamaa zenu. Ninasema hivi ili kuwaruhusu mtengane kwa muda tu. Lakini hii siyo amri. Mimi ningependa kila mtu angekuwa kama mimi nilivyo. Lakini Mungu amempa kila mtu uwezo tofauti. Huwafanya wengine kuwa hivi na wengine kuwa vile. Sasa kwa ajili ya wale ambao hawajaoa ama hawajaolewa na kwa ajili ya wajane ninawaambia ya kwamba ni vizuri mkae bila kuoa au kuolewa kama mimi. Lakini ikiwa mtashindwa kudhibiti tamaa zenu, basi mwoe au muolewe. Ni vyema kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa. Na sasa ninawaamuru wale walio katika ndoa. Si amri kutoka kwangu, lakini ndivyo Bwana aliamuru. Mke hapaswi kuondoka kwa mume wake. Lakini ikiwa mke anaondoka, anapaswa kukaa bila kuolewa au arudi kwa mume wake. Na mume hapaswi kumtaliki mke wake. Ushauri nilionao kwa wengine unatoka kwangu. Bwana hajatupa mafundisho mengine kuhusu hili. Ukiwa na mke asiyeamini, usimtaliki ikiwa yuko radhi kuendelea kuishi pamoja nawe. Na kama una mume asiyeamini, usimtaliki ikiwa yuko radhi kuendelea kuishi pamoja nawe. Mume asiyeamini ametengwa kwa ajili ya Bwana kupitia mke wake anayeamini. Na mke asiyeamini ametengwa kwa ajili ya Bwana kupitia mume wake anayeamini. Ikiwa hii si sahihi basi watoto wenu wasingefaa kwa ajili ya kumwabudu Mungu. Lakini sasa wametengwa kwa ajili yake. Lakini mume au mke asiyemwamini akiamua kuondoka katika ndoa. Hili linapotokea, ndugu aliye katika Kristo anakuwa huru. Mungu aliwachagua ili muwe na maisha ya amani. Inawezekana ninyi wake mtawaokoa waume zenu; nanyi waume mtawaokoa wake zenu kwani bado hamjui kitakachotokea baadaye. Kila mmoja wenu anapaswa kuendelea kuishi katika namna ambayo Bwana Mungu amewapa, kuishi kama mlivyoishi Mungu alipowaita. Ninawaambia watu katika makanisa yote kufuata kanuni hii. Mwanaume asibadili tohara yake ikiwa alikuwa ametahiriwa alipoitwa. Ikiwa hakuwa ametahiriwa alipoitwa, asitahiriwe. Kutahiriwa au kutotahiriwa si muhimu. Kilicho muhimu ni kutii amri za Mungu. Kila mmoja wenu awe katika hali aliyokuwa nayo Mungu alipomwita. Usijisikie vibaya ikiwa ulipochaguliwa na Mungu ulikuwa mtumwa. Lakini ikiwa unaweza kujikomboa, basi fanya hivyo. Kama ulikuwa mtumwa Bwana alipokuita, uko huru sasa katika Bwana. Wewe ni wa Bwana. Vivyo hivyo, kama ulikuwa huru ulipoitwa, wewe ni mtumwa wa Kristo sasa. Mungu alilipa gharama kubwa kwa ajili yako, hivyo usiwe mtumwa kwa mtu yeyote tena. Ndugu zangu, katika maisha yenu mapya pamoja na Mungu, kila mmoja wenu anapaswa kuendelea kuwa katika hali ya tohara kama alivyokuwa Mungu alipowaita. Sasa nitaandika kuhusu suala jingine mliloniandikia mkiuliza kuhusu watu ambao hawajaoa au kuolewa. Sina amri kutoka kwa Bwana kuhusu hili, lakini haya ni maoni yangu. Na ninaweza kuaminiwa kwa sababu Bwana amenipa rehema. Huu ni wakati mgumu. Hivyo nadhani ni vyema mtu akikaa kama alivyo. Ikiwa umefungwa kwa mke, usijaribu kufunguliwa. Ikiwa hujaoa, usijaribu kuoa. Lakini si dhambi ukiamua kuoa. Lakini waliooa watapata dhiki katika maisha haya, nami ninataka msiipitie dhiki hiyo. Kaka zangu nina maana ya kuwa muda uliosalia ni mchache, wale waliooa waishi kama vile hawajaoa. Wale wanaolia wawe kama wasiolia, wenye furaha wawe kama hawana furaha na wale wanaonunua vitu wawe kama hawavimiliki vitu hivyo. Vitumieni vitu vya ulimwengu pasipo kuviruhusu viwe vya muhimu kwenu. Hivi ndivyo mnapaswa kuishi, kwa sababu ulimwengu huu kwa namna ulivyo sasa, unapita. Nataka msisumbuke. Mwanaume ambaye hajaoa hujishughulisha na kazi ya Bwana naye hujitahidi kumpendeza Bwana. Lakini mwanaume aliyeoa hujishughulisha na mambo ya ulimwengu, ili ampendeze mke wake. Ni lazima afikirie mambo mawili; kumpendeza mke wake na kumpendeza Bwana. Mwanamke ambaye hajaolewa au msichana ambaye hajawahi kuolewa hujishughulisha na kazi ya Bwana. Hutaka kuutoa mwili na roho yake kikamilifu kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya ulimwengu ili ampendeze mume wake. Ninasema hili ili niwasaidie. Si kuwawekea vikwazo, lakini ninataka mwishi katika njia sahihi. Na ninataka mjitoe kikamilifu kwa Bwana pasipo kuchukuliwa katika mambo mengine. Mwanaume anaweza kudhani kuwa hamtendei haki mchumba wake. Mchumba wake huyo anaweza kuwa ameshapita umri mzuri wa kuolewa. Hivyo mwanaume anaweza kujisikia kuwa anapaswa kumwoa mchumba wake huyo. Basi na afanye anachotaka. Si dhambi kwao wakioana. Lakini mwanaume mwingine anaweza kuwa na uhakika akilini mwake ya kuwa hakuna haja ya ndoa, hivyo yuko huru kufanya anachotaka. Ikiwa ameamua moyoni mwake kutomwoa mchumba wake, anafanya jambo sahihi. Hivyo mwanaume anayemwoa mchumba wake anafanya jambo jema, na mwanaume asiyeoa anafanya vyema zaidi. Mwanamke anapaswa kuishi na mume wake kipindi chote mumewe anapokuwa hai. Lakini mume akifa, mwanamke anakuwa huru kuolewa na mwanaume yeyote. Lakini mwanaume huyo lazima awe yule wa Bwana. Ikiwa atabaki kuwa mjane, atakuwa na furaha sana. Haya ni maoni yangu, na ninaamini yanatoka kwa Roho wa Mungu. Sasa nitaandika kuhusu suala jingine mliloniandikia mkiuliza kuhusu nyama iliyotolewa sadaka kwa sanamu. Ni kweli kuwa “Sote tuna ujuzi”, kama mnavyosema. Lakini ujuzi huu unawajaza watu majivuno. Upendo ndiyo unaolisaidia kanisa kuwa imara. Wale wanaodhani kuwa wanajua jambo fulani bado hawajui chochote kwa namna inavyopaswa. Lakini Mungu anamjua mtu anayempenda. Hivyo sasa vipi kuhusu kula nyama iliyotolewa sadaka kwa sanamu? Tunajua kuwa “sanamu si lolote katika ulimwengu” huu na tunajua kuwa “kuna Mungu mmoja tu”. Baadhi ya watu husema kuwa kuna miungu wanaoishi mbinguni na miungu wengine huishi duniani. Hata kama kuna “miungu” na “mabwana” wanaoaminiwa na watu, hilo si muhimu kwetu. Tuna Mungu mmoja tu, na ambaye ndiye Baba yetu. Vitu vyote vilitoka kwake nasi tunaishi kwa ajili yake. Na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo. Vitu vyote viliumbwa kupitia yeye, nasi tunaishi kwa ajili yake. Lakini si watu wote wanaojua hili. Baadhi ya watu walikuwa na tabia ya kuabudu sanamu huko nyuma. Hivyo wanapokula nyama, bado wanahisi kuhukumiwa kana kwamba wanakula nyama iliyotolewa kwa sanamu. Hawana uhakika ikiwa ni sahihi kula nyama. Lakini chakula hakitatuweka karibu na Mungu. Kukataa kula hakutufanyi tumpendeze kidogo Mungu wala kula hakutuweki karibu na Mungu. Lakini iweni makini na uhuru wenu. Uhuru wa kula kitu unaweza kuwafanya walio na mashaka wakaanguka katika dhambi kwa kula vyakula hivyo. Mnaelewa kuwa inaruhusiwa kula kitu chochote, hivyo unaweza kula hata katika hekalu la sanamu. Lakini hilo linaweza kumfanya mtu mwenye mashaka akaona kuwa kula chakula kama hicho ni kitendo cha kuabudu sanamu. Hivyo ndugu huyu aliye dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, anaweza akaangamizwa kwa sababu ya uelewa wako ulio mzuri zaidi. Unapomtenda dhambi kinyume cha ndugu zako walio katika Kristo kwa namna hii na unawaumiza kwa kuwafanya wafanye mambo wanayoyachukulia kuwa mabaya, nawe pia unamtenda dhambi Kristo. Hivyo ikiwa chakula ninachokula kinamfanya mwamini mwingine kutenda dhambi, siwezi kula chakula hicho tena. Nitaacha kula chakula hicho ili nisimfanye ndugu yangu atende dhambi. Mnajua kuwa mimi ni mtu niliye huru. Mnajua kuwa mimi ni mtume na kwamba nilimwona Yesu Bwana wetu. Na ninyi ni kielelezo cha kazi yangu katika Bwana. Wengine wanaweza wasikubali kuwa mimi ni mtume, lakini hakika ninyi mnakubali. Ninyi ni uthibitisho kuwa mimi ni mtume wa Bwana. Ninataka kuwajibu baadhi ya watu wanaotaka kunichunguza. Je, hatuna haki ya kula na kunywa? Je, hatuna haki ya kusafiri pamoja na mke aliye mwamini? Mitume wengine wote, wadogo zake Bwana na Petro hufanya hivi. Na je, ni mimi na Barnaba tu ndiyo ambao ni lazima tufanya kazi ili tupate kipato cha kutuwezesha kuishi? Ni askari gani aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi la kondoo na hanywi maziwa? Lakini nina mifano mingi kutoka katika maisha ya kila siku inayosisitiza hoja yangu. Sheria ya Mungu inasema vivyo hivyo pia. Ndiyo, imeandikwa katika Sheria ya Musa kuwa; “Mnyama wa kazi anapotumika kupura nafaka, usimzuie kula nafaka.” Je, Mungu aliposema hivi, alikuwa anawawazia wanyama pekee? Hapana. Hakika Mungu alizungumza kuhusu sisi. Ndiyo, iliandikwa kwa ajili yetu. Wote wawili, anayelima na anayepura nafaka, wana haki ya kupata nafaka kutokana na kazi yao. Ikiwa tulipanda mbegu ya kiroho mioyoni mwenu, je, hatustahili kupata vitu kwa ajili ya maisha haya kutoka kwenu? Ikiwa wengine wana haki ya kupata vitu kutoka kwenu, hakika hata sisi tuna haki pia. Lakini hatuitumii haki hii. Tunavumilia katika hali zote ili tusimfanye mtu yeyote akaacha kuitii Habari Njema ya Kristo. Hakika mnajua ya kuwa wanaotumika Hekaluni hula chakula kutoka Hekaluni. Na wale wanaotumika madhabahuni hupata sehemu ya yale yanayotolewa madhabahuni. Vivyo hivyo kwa wale wenye kazi ya kuhubiri Injili. Bwana ameamuru kuwa nao wataishi kutokana na kazi hiyo. Lakini sijatumia haki hizi, na si kwamba ninataka kitu chochote kutoka kwenu. Ijapokuwa ninaandika hivi hilo si lengo langu. Ni bora nife kuliko mtu yeyote kuchukua kutoka kwangu kitu ninachojivunia. Sijivuni kwa sababu ya kazi yangu ya kuhubiri Habari Njema kwa sababu ni wajibu wangu ambao ni lazima nifanye; ole wangu nisipowahubiri watu Habari Njema. Ikiwa ningehubiri kwa sababu ya utashi kwangu, ningestahili kulipwa. Lakini sikuchagua kufanya kazi hii. Ni lazima nihubiri Habari Njema. Hivyo ninafanya kazi niliyokabidhiwa. Sasa, kwa kufanya kazi hii ninapata nini? Thawabu yangu, ni kuwa ninapowahubiri watu Habari Njema, ninawapa bure na sizitumii haki zinazoambatana na kufanya kazi hii. Niko huru. Similikiwi na mtu yeyote, lakini ninakuwa mtumwa ili watu wengi waokoke. Kwa Wayahudi nilienenda kama Myahudi ili nisaidie Wayahudi wengi waokolewe. Sitawaliwi na sheria, lakini kwa wanaotawaliwa na sheria nilikuwa kama ninayetawaliwa na sheria. Nilifanya hivi kuwasaidia wanaotawaliwa na sheria, ili waokoke. Kwa wasio na sheria nilikuwa kama nisiye na sheria, ili niwasaidie wasio na sheria kuokoka. Mimi si kama mtu asiye na Sheria ya Mungu, ninatawaliwa na sheria ya Kristo. Kwa waliodhaifu, nilikuwa dhaifu ili niwasaidie kuokoka. Nilifanyika kila kitu kwa watu wote ili nifanye kila kinachowezekana niweze kuwasaidia watu waokolewe. Ninafanya kila ninachoweza ili Habari Njema ijulikane na niweze kushiriki katika Habari zake. Mnajua kuwa katika riadha, wanariadha wengi hukimbia, lakini mmoja tu hupata zawadi. Hivyo kimbieni hivyo. Kimbieni ili mshinde! Wote wanaoshiriki katika mchezo hufanya mazoezi kwa bidii ili waweze kushinda na kupata zawadi. Lakini zawadi wanazopata hazidumu milele. Lakini zawadi yetu ni ile inayodumu milele. Hivyo ninakimbia kama mtu mwenye malengo. Ninapigana ngumi kama mpiganaji anayepiga kitu, si kama anayepiga hewa. Ninaudhibiti mwili wangu kikamilifu na kuufanya unitiii kwa kila jambo ninalotaka kutenda. Ninafanya hivi ili mimi binafsi nisiikose thawabu baada ya kuwahubiri wengine Habari Njema. Ndugu zangu, sitaki mshindwe kutambua umuhimu wa kile kilichowatokea baba zetu waliokuwa na Musa. Walifunikwa na wingu, na walipita katika bahari. Walibatizwa wote katika Musa katika wingu na katika bahari. Wote walikula chakula kilichotolewa na Roho wa Mungu, na wote walikunywa kinywaji kinachotolewa na Roho wa Mungu. Kinywaji walichokunywa kilitoka katika mwamba wa roho uliokuwa pamoja nao, na mwamba huo ni Kristo. Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, na hivyo waliangamizwa jangwani. Mambo haya yaliyotokea ni tahadhali kwa ajili yetu. Mifano hii itufanye tuache kutamani maovu kama baadhi yao walivyofanya. Msiabudu sanamu kama ambavyo baadhi yao walifanya. Na kama Maandiko yanavyosema, “Waliketi chini kula na kunywa kisha wakasimama kucheza.” Tusifanye dhambi ya uzinzi kama baadhi yao walivyofanya na watu ishirini na tatu elfu miongoni mwao wakafa. Tusimjaribu Kristo kama vile baadhi yao walivyofanya. Kwa sababu hiyo, waliuawa na nyoka. Na msinung'unike kama baadhi yao walivyofanya na wakauawa na malaika anayeangamiza. Mambo yaliyowapata wale watu ni mifano na yaliandikwa ili kututahadharisha sisi tunaoishi nyakati hizi za mwisho. Hivyo kila anayedhani kuwa yuko imara katika imani yake, basi awe mwangalifu asianguke. Majaribu mliyonayo ni yale yale waliyonayo watu wote. Lakini Mungu ni mwaminifu maana hataacha mjaribiwe kwa kiwango msichoweza kustahimili. Mnapojaribiwa, Mungu atawapa mlango wa kutoka katika jaribu hilo. Ndipo mtaweza kustahimili. Hivyo rafiki zangu wapenzi, zikimbieni ibada za sanamu. Ninyi ni watu wenye akili. Upimeni ukweli wa haya ninayosema sasa. Kikombe cha baraka tunachokitolea shukrani ni ushirika wa sadaka ya damu ya Kristo, sawa? Na mkate ule tunaomega, ni ushirika wa mwili wa Kristo, sawa? Kuna mkate mmoja, nasi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa tunashiriki katika mkate huo mmoja. Na fikirini kuhusu Waisraeli wanavyofanya. Wanapokula sadaka, wanaunganishwa pamoja kwa kugawana kile kilichotolewa kwenye madhabahu. Je, ninataka kuthibitisha kitu gani? Je, ninasema kwamba nyama iliyotolewa sadaka kwa sanamu ni hakika najisi kwa kiasi fulani? Je, ninasema kwamba sanamu ni mungu wa kweli? Hapana. Lakini ninasema kuwa chakula kinapotolewa sadaka kwa sanamu, ni sadaka kwa mashetani, siyo kwa Mungu. Nami sitaki ninyi muungane na hao wengine katika kuyaabudu mashetani. Hamwezi kukinywea kikombe cha Bwana na kisha mkakinywea kiombe kinachotukuza mashetani. Hamwezi kushiriki kula chakula na kunywa pamoja kwenye meza ya Bwana kisha mkaenda kushiriki kula chakula na kunywa pamoja kwenye meza inayotukuza mashetani. Kufanya hivyo kunamtia wivu Bwana. Je, mnafikiri tunaweza kujaribu kumfanya Bwana apate wivu? Mnadhani tuna nguvu kuliko yeye? Mnasema “Vitu vyote vimeruhusiwa.” Lakini si vitu vyote vinafaa. “Vitu vyote vimeruhusiwa.” Lakini vitu vingine havisaidii katika kuliimarisha kanisa. Jitahidi kuwafanyia mema wengine badala ya kufanya mema kwa ajili yako wewe wenyewe. Kuleni chakula chochote kinachouzwa sokoni. Msiulize maswali ili kutafuta kujua kama ni sahihi ama la kwako kukila. Mnaweza kula chakula hicho, “Kwa sababu dunia na kila kitu kilichomo ndani yake ni vya Bwana.” Asiye mwamini anaweza kuwaalika kula chakula. Ikiwa mtakwenda, basi mle chochote kitakachowekwa mbele yenu. Msiulize ulize maswali. Lakini mtu akiwaambia, “Chakula hicho kilitolewa sadaka katika hekalu la miungu,” basi msile. Kwa sababu kinaweza kumwathiri mtu na uhusiano wake na Mungu. Na hapa sizungumzii kuhusu uhusiano wenu na Mungu, bali uhusiano wa mtu yule aliyewaambia na Mungu. Kwa nini uhuru wangu mwenyewe uhukumiwe na mawazo ya mtu mwingine? Ikiwa mimi nitakula chakula nikiwa na shukrani, kwa nini basi nisikosolewa kwa sababu ya kitu ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu? Ninachosema ni kwamba: ukila, au ukinywa, au ukifanya jambo lolote, lifanye kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Kamwe usifanye jambo lolote litakalowafanya watu wengine kutenda mabaya, iwe ni Wayahudi, wasio Wayahudi au mtu yeyote katika kanisa la Mungu. Ninafanya vivyo hivyo. Ninajitahidi kwa njia yeyote ile kumpendeza kila mtu. Mimi sijaribu kutenda yaliyo mema kwangu. Ninajaribu kutenda yale yaliyo na manufaa kwa watu wengine ili waweze kuokoka. Fuateni mfano wangu, kama ninavyoufuata mfano wa Kristo. Nawasifu kwa sababu daima mnanikumbuka mimi na kuyafuata mafundisho niliyowapa. Lakini ninataka mwelewe kuwa kichwa cha kila mwanaume ni Kristo. Na Kichwa cha mwanamke ni mwanaume. Na Kichwa cha Kristo ni Mungu. Kila mwanaume anayeomba au kutabiri akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake. Lakini kila mwanamke anayeomba au kutabiri pasipo kufunika kichwa chake anakiaibisha kichwa chake. Kwa jinsi hiyo anakuwa sawa na mwanamke yule aliyenyoa nywele zake. Ikiwa mwanamke hatafunika kichwa chake, basi na azinyoe nywele zake. Lakini ni aibu kwa mwanamke kukata nywele zake au kuzinyoa kichwani mwake. Hivyo anapaswa kufunika kichwa chake. Lakini mwanaume hapaswi kufunika kichwa chake, kwa sababu ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume. Mwanaume hakutoka kwa mwanamke bali mwanamke ndiye aliyetoka kwa mwanaume. Na mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke lakini mwanamke ndiye aliumbwa kwa ajili ya mwanaume. Hivyo, kutokana na nilivyosema, mwanamke anapaswa kukitawala kichwa chake kwa kukifunika anapoomba au anapotabiri. Pia, anapaswa kufanya hivi kwa sababu ya malaika. Lakini katika Bwana mwanamke anamhitaji mwanaume, na mwanaume anamhitaji mwanamke. Hii ni kweli kwa sababu mwanamke alitoka kwa mwanaume, lakini pia mwanaume anazaliwa na mwanamke. Hakika, kila kitu kinatoka kwa Mungu. Amueni hili ninyi wenyewe: Je, ni sahihi mwanamke kumwomba Mungu akiwa hajafunika kichwa chake? Je, si hata hali ya asili inatufundisha kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu? Lakini kuwa na nywele ndefu ni heshima kwa mwanamke. Mwanamke amepewa nywele ndefu ili kufunika kichwa chake. Baadhi ya watu wanaweza kuanzisha mabishano kuhusiana na yale niliyosema. Lakini desturi ambayo sisi na makanisa ya Mungu yanafuata ni hii: ya kwamba wanawake wanaweza kuomba na kutabiri ujumbe kutoka kwa Mungu, vichwa vyao vikiwa vimefunikwa. Siwasifu kwa mambo ninayowaambia sasa. Mikutano yenu inawaumiza kuliko inavyowasaidia. Kwanza, nimesikia kuwa mnapokutana kama kanisa mmegawanyika. Hili si gumu kuliamini kwa sababu ya fikra zenu kwamba imewapasa kuwa na makundi tofauti ili kuonesha ni akina nani walio waamini wa kweli! Mnapokusanyika, hakika hamli chakula cha Bwana. Ninasema hivi kwa sababu mnapokula, kila mmoja anakula na kumaliza chakula chake pasipo kula na wengine. Baadhi ya watu hawapati chakula cha kutosha, ama kinywaji cha kutosha na hivyo kubaki na njaa na kiu, ambapo wengine wanakula na kunywa zaidi hata kulewa. Mnaweza kula na kunywa katika nyumba zenu. Inaonekana kuwa mnadhani kanisa la Mungu si muhimu. Mnawatahayarisha wasio na kitu. Niseme nini? Je, niwasifu? Hapana, siwezi kuwasifu katika hili. Mafundisho niliyowafundisha ni yale yale niliyopokea kutoka kwa Bwana, ya kwamba usiku ule ambao Bwana Yesu alikamatwa, aliuchukua mkate na akashukuru. Kisha akaumega na kusema, “Huu ni mwili wangu; ni kwa ajili yenu. Uleni mkate huu kwa ajili ya kunikumbuka mimi.” Kwa namna hiyo hiyo, baada ya wote kula, Yesu alichukua kikombe cha divai na akasema, “Divai hii inawakilisha agano jipya ambalo Mungu anafanya na watu wake, linaloanza kwa sadaka ya damu yangu. Kila mnywapo divai hii, fanyeni hivi kwa ajili ya kunikumbuka mimi.” Hii inamaanisha kuwa kila mnapokula mkate huu na kunywa kikombe hiki, mnawaambia wengine kuhusu kifo cha Bwana mpaka atakaporudi. Hivyo, ukiula mkate na kukinywea kikombe cha Bwana isivyostahili, unautendea dhambi mwili na damu ya Bwana. Unapaswa kujichunguza mwenendo wako kabla ya kula mkate na kunywa kikombe. Ukila na kunywa bila kuwajali wale ambao ndiyo mwili wa Bwana, kula na kunywa kwako kutasababisha uhukumiwe kuwa mwenye hatia. Ndiyo sababu watu wengi katika kanisa lenu ni wagonjwa na dhaifu, na wengi wameshakufa. Lakini ikiwa tungejichunguza kwa usahihi, Mungu asingetuhukumu. Lakini Bwana anapotuhukumu, anatuadhibu ili kutuonesha njia sahihi. Hufanya hivi ili tusishutumiwe kuwa wakosa na tukahukumiwa pamoja na ulimwengu. Hivyo ndugu zangu, mnapokusanyika pamoja ili mle, subirianeni na mkaribishane kwa moyo wa upendo. Ikiwa mtu yeyote anawaza kuhusu njaa yake mwenyewe, basi akae nyumbani kwake na ale huko! Fanyeni hivi ili kukutanika kwenu kusilete hukumu ya Mungu juu yenu. Nitakapokuja nitawaambia nini cha kufanya kuhusu masuala mengine. Na sasa ninataka mwelewe kuhusu karama za Roho Mtakatifu. Mnayakumbuka maisha mliyoishi kabla hamjawa waamini. Mlipotoshwa na kuongozwa kuziabudu sanamu, ambazo hata kuzungumza haziwezi. Hivyo ninawaambia ya kwamba hakuna mtu anayezungumza kwa Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu alaaniwe.” Na hakuna anayeweza kusema “Yesu ni Bwana,” bila msaada wa Roho Mtakatifu. Kuna karama mbalimbali za Roho, lakini zote zinatoka kwa Roho yule yule. Kuna namna mbalimbali za kutumika, lakini sote tunatumika kwa niaba ya Bwana yule yule. Na kuna namna ambazo Mungu hufanya kazi ndani yetu sote, lakini ni Mungu yule yule anayetenda kazi ndani yetu ili tutende kila kitu. Kitu fulani kutoka kwa Roho kinaweza kuonekana ndani ya kila mtu. Roho humpa kila mtu hili ili awasaidie wengine. Roho humpa mtu fulani uwezo wa kuzungumza kwa hekima. Na Roho huyo huyo humpa mwingine uwezo wa kuzungumza kwa maarifa. Roho huyo huyo humpa mtu karama ya imani na humpa mwingine karama ya kuponya. Roho humpa mtu nguvu ya kutenda miujiza, na humpa mwingine uwezo wa kutabiri, na mwingine uwezo wa kupambanua kujua kilichotoka kwa Roho na ambacho hakikutoka kwa Roho. Roho humpa mtu fulani uwezo wa kusema kwa lugha zingine tofauti, na humpa mwingine uwezo wa kufasiri lugha hizo. Roho mmoja, Roho yule yule hufanya mambo yote haya. Roho ndiye huamua ampe nini kila mtu. Mtu ana mwili mmoja, lakini una viungo vingi. Kuna viungo vingi, lakini viungo vyote hivyo ni mwili mmoja. Kristo yuko vivyo hivyo pia. Baadhi yetu ni Wayahudi na baadhi yetu si Wayahudi; baadhi yetu ni watumwa na baadhi yetu ni watu tulio huru. Lakini sisi sote tulibatizwa ili tuwe sehemu ya mwili mmoja kwa njia ya Roho mmoja. Nasi tulipewa Roho mmoja. Na mwili wa mtu una viungo zaidi ya kimoja. Una viungo vingi. Mguu unaweza kusema, “Mimi si mkono, na hivyo mimi si wa mwili.” Lakini kusema hivi hakutafanya mguu usiwe kiungo cha mwili. Sikio linaweza kusema, “Mimi si jicho, hivyo mimi si wa mwili.” Lakini kwa kusema hivi hakutafanya sikio lisiwe kiungo cha mwili. Ikiwa mwili wote ungekuwa jicho, usingeweza kusikia. Ikiwa mwili wote ungekuwa sikio, usingeweza kunusa kitu chochote. Ikiwa viungo vyote vya mwili vingekuwa kiungo kimoja, mwili usingekuwepo. Kama jinsi ilivyo, Mungu aliweka viungo katika mwili kama alivyotaka. Alikipa kila kiungo sehemu yake. *** Hivyo kuna viungo vingi, lakini kuna mwili mmoja tu. Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sikuhitaji!” Na kichwa hakiwezi kuuambia mguu, “sikuhitaji!” Hapana, viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu zaidi, ndivyo vilivyo na umuhimu zaidi. Na viungo ambavyo tunadhani kuwa vina umuhimu mdogo ndivyo tunavitunza kwa heshima kubwa. Na tunavitunza kwa kuvifunika kwa uangalifu maalum viungo vya mwili tusivyotaka kuvionesha. Viungo vinavyopendeza zaidi visipofunikwa havihitaji matunzo haya maalum. Lakini Mungu aliuunganisha mwili pamoja na akavipa heshima zaidi viungo vilivyohitaji hadhi hiyo. Mungu alifanya hivi ili mwili wetu usigawanyike. Mungu alitaka viungo vyote tofauti vitunzane kwa usawa. Ikiwa kiungo kimoja cha mwili kinaugua, basi viungo vyote vinaugua pamoja nacho. Au ikiwa kiungo kimoja kinaheshimiwa, basi viungo vingine vyote vinashiriki heshima ya kiungo hicho. Ninyi nyote kwa pamoja ni mwili wa Kristo. Kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo. Na Mungu ameweka katika kanisa, kwanza, baadhi kuwa mitume, pili manabii, na tatu walimu. Kisha Mungu ametoa nafasi kwa wale wanaofanya miujiza, wenye karama ya uponyaji, wanaoweza kuwasaidia wengine, wanaoweza kuwaongoza wengine na wale wanaoweza kuzungumza kwa lugha zingine. Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote hufanya miujiza? Si wote wenye karama ya uponyaji. Si wote wanaozungumza kwa lugha zingine. Si wote wanaofasiri lugha. Endeleeni kuwa na ari ya kuwa na karama za Roho mnazoona kuwa ni kuu zaidi. Lakini sasa ninataka kuwaonesha njia iliyo kuu zaidi. Ninaweza kusema kwa lugha zingine, za wanadamu au za malaika. Lakini ikiwa sina upendo, mimi ni kengele yenye kelele na tuazi linalolia. Ninaweza kuwa na karama ya unabii, ninaweza kuzielewa siri zote na kujua kila kitu kinachopaswa kujulikana, na ninaweza kuwa na imani kuu kiasi cha kuhamisha milima. Lakini pamoja na haya yote, ikiwa sina upendo, mimi ni bure. Ninaweza kutoa kila kitu nilichonacho ili niwasaidie wengine na ninaweza hata kuutoa mwili wangu ili niweze kujisifu. Lakini siwezi kupata chochote kwa kufanya haya yote ikiwa sina upendo. Upendo huvumilia na ni mwema. Upendo hauna wivu, haujisifu na haujivuni. Upendo hauna kiburi, hauna ubinafsi na haukasirishwi kirahisi. Upendo hautunzi orodha ya mambo waliyoukosea. Upendo haufurahi wengine wanapokosa, lakini daima hufurahia ukweli. Upendo kamwe haukati tamaa kwa watu. Kamwe hauachi kuamini, kamwe haupotezi tumaini na kamwe hauachi kuvumilia. Upendo hautakoma. Lakini karama zote hizo zitafikia mwisho, hata karama ya unabii, karama ya kusema kwa lugha zingine na karama ya maarifa. Hizi zitakoma kwa sababu maarifa haya na nabii hizi tulizonazo sasa hazijakamilika. Lakini ukamilifu utakapokuja, mambo ambayo hayajakamilika yatakoma. Nilipokuwa mtoto, nilizungumza kama mtoto, niliwaza kama mtoto, na kufanya mipango kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima, niliziacha njia za kitoto. Ndivyo ilivyo hata kwetu. Kwa sasa tunamwona Mungu kwa taswira tu kama ilivyo katika kioo. Lakini, baadaye, tutamwona uso kwa uso. Kwa sasa ninajua sehemu tu, lakini wakati huo nitajua kila kitu, kama ambavyo Mungu amenijua mimi. Hivyo mambo haya matatu yanaendelea; imani, tumaini na upendo. Na lililo kuu zaidi ya haya yote ni upendo. Upendo uwe lengo la maisha yenu, lakini mnapaswa pia kuzitaka karama za Roho. Na itakeni sana karama ya unabii. Nitafafanua ni kwa nini. Wenye karama ya kusema kwa lugha zingine hawazungumzi na watu. Huzungumza na Mungu. Hakuna anayewaelewa kwa sababu huzungumza mambo ya siri kupitia Roho. Lakini wanaotabiri huzungumza na watu. Huwasaidia watu kuwa imara katika imani, na huwatia moyo na kuwafariji. Wanaosema kwa lugha hujiimarisha wao wenyewe. Lakini wanaotabiri huliimarisha kanisa lote. Ningependa ninyi nyote muwe na karama ya kusema kwa lugha zingine. Lakini ninachotaka zaidi ni ninyi kutabiri. Yeyote anayetabiri ni wa muhimu zaidi kuliko wale wanaosema kwa lugha zingine. Hata hivyo, ikiwa wanaweza kufasiri lugha hizo, basi kanisa linasaidiwa kutokana na kile wanachosema. Ndugu zangu, je, itawasaidia nikija kwenu na kusema kwa lugha zingine? Hapana, itawasaidia pale tu nitakapowaletea ufunuo mpya au maarifa fulani, unabii au mafundisho. Hii ni kweli hata kwa vitu visivyo na uhai vinavyotoa sauti kama filimbi na kinubi. Ikiwa muziki hauchezwi kwa ufasaha, hutaweza kujua ni wimbo gani unaopigwa. Na katika vita, ikiwa tarumbeta haitatoa ishara vizuri, askari hawawezi kujua kuwa ni wakati wa kujiandaa kwa mapigano. Ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi. Watu hawataweza kuelewa unachosema, ikiwa utazungumza katika lugha tofauti wasiyoitambua. Utakuwa unazungumza hewani tu! Ni dhahiri kuwa kuna lugha nyingi ulimwenguni, na zote zina maana. Lakini ikiwa sielewi maana ya maneno wanayosema wengine, kwangu itakuwa sauti ya ajabu tu, na nitasikika kama ninayetoa sauti za ajabu. Kwa kuwa mna nia kuhusu karama za Kiroho, muwe na hamu ya kulisaidia kanisa kuwa imara. Hivyo wenye karama ya kusema kwa lugha waombe ili waweze kufasiri yale wanayosema. Ninapoomba kwa lugha zingine, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haifanyi chochote. Hivyo nifanye nini? Nitaomba kwa roho yangu, lakini pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho yangu, lakini pia nitaimba kwa akili yangu. Unaweza ukawa unamshukuru Mungu kwa roho yako. Lakini mtu mwingine ambaye haielewi lugha unayotumia hawezi kusema “Amina” kwa maombi yako ya shukrani. Unaweza ukawa unamshukuru Mungu katika njia nzuri, lakini isiwasaidie wengine kuwa imara. Ninamshukuru Mungu kwamba nimepewa karama ya kusema lugha aina nyingi mbalimbali kuliko yeyote kati yenu. Lakini wakati wa mikutano ya kanisa napenda kuzungumza maneno matano ninayoyaelewa kuliko maelfu ya maneno katika lugha zingine. Ni afadhali nizungumze nikiwa katika uelewa wangu ili niwafundishe wengine. Ndugu zangu, msiwaze kama watoto wadogo. Iweni kama watoto wachanga katika mambo maovu, lakini katika kuwaza kwenu muwe kama watu wazima, waliokua. Kama Maandiko yanavyosema, “Kwa kutumia wanaozungumza lugha tofauti na kutumia midomo ya wageni, nitazungumza na watu hawa, hata hivyo, hawatanitii.” Hivi ndivyo Bwana anasema. Na kutokana na hili tunaona kwamba matumizi ya lugha zingine ni ishara kuonesha namna ambavyo Mungu anawashughulikia wasioamini, na si walioamini. Na unabii unaonesha namna ambavyo Mungu hutenda kazi kupitia wanaoamini, na si wasioamini. Chukulieni kuwa kanisa lote limekusanyika nanyi nyote mkaanza kusema kwa lugha zingine. Ikiwa baadhi ya watu wasio sehemu ya kundi lenu au wasio waamini wataingia katika kusanyiko lenu, watasema ninyi ni wendawazimu. Lakini chukulieni kuwa ninyi nyote mnatabiri na mtu asiyeamini ama asiyekuwa sehemu ya kundi lenu akaingia. Dhambi zao zitawekwa wazi kwao, na watahukumiwa kwa kila kitu mtakachosema. Mambo ya siri katika mioyo yao yatajulikana. Na watapiga magoti na kumwabudu Mungu. Watakiri na kusema, “Pasipo shaka, Mungu yuko hapa pamoja nanyi.” Basi ndugu, mnapaswa kufanya nini? Mnapokusanyika, mtu mmoja ana wimbo, mwingine ana mafundisho na mwingine ana kweli mpya kutoka kwa Mungu. Mmoja anasema kwa lugha nyingine na mwingine anafasiri lugha hiyo. Cho chote mnachofanya lazima kiwe na lengo la kumfanya kila mmoja wenu akue katika imani. Mnapokusanyika, ikiwa kuna yeyote atasema na kanisa katika lugha, iwe watu wawili tu au isiwe zaidi ya watu watatu. Na wanapaswa wanene kwa zamu, mmoja baada ya mwingine. Na mwingine afasiri kile wanachosema. Lakini ikiwa hakuna mfasiri, basi mtu yeyote anayesema kwa lugha nyingine anapaswa kunyamaza kimya. Wanapaswa kuzungumza katika nafsi zao wenyewe ama na Mungu. Na manabii wawili au watatu tu ndiyo wanapaswa kuzungumza. Wengine watathmini kile wanachosema. Na ujumbe kutoka kwa Mungu ukimjia mtu aliyekaa, mzungumzaji wa kwanza anapaswa kunyamaza. Nyote mnaweza kutabiri mmoja baada ya mwingine. Kwa njia hii kila mmoja anaweza kufundishwa na kutiwa moyo. Roho za manabii ziko chini ya udhibiti wa manabii wenyewe. Mungu si Mungu wa machafuko lakini ni Mungu wa amani. Hii ni kanuni kwa ajili ya mikutano yote ya watu wa Mungu. Wanawake wanapaswa kunyamaza katika mikutano hii ya kanisa. Kama Sheria ya Musa inavyosema, hawaruhusiwi kuzungumza pasipo utaratibu bali wawe chini ya mamlaka. Wakiwa na jambo wanalotaka kujua, wawaulize waume zao nyumbani. Ni aibu kwa mwanamke kuzungumza pasipo utaratibu katika mikutano ya kanisa. Je, ni kutoka kwenu neno la Mungu lilikuja ama lilikuja kwa ajili yenu pekee? Ikiwa yeyote kati yenu anafikiri kuwa yeye ni nabii au kwamba ana karama ya kiroho, anapaswa kuelewa kuwa ninachowaandikia ninyi nyote ni amri ya Bwana. Ikiwa yeyote miongoni mwenu hatalikubali hili, basi hatakubaliwa. Hivyo ndugu zangu, mzingatie sana kutabiri. Na msimzuie mtu yeyote kutumia karama ya kusema katika lugha zingine. Lakini kila kitu kifanywe kwa usahihi na kwa utaratibu. Sasa ndugu zangu, ninataka mkumbuke Habari Njema niliyowahubiri. Mliupokea ujumbe huo na endeleeni kuishi kwa kuufuata. Habari Njema hiyo, ujumbe mliousikia kutoka kwangu, ni njia ya Mungu kuwaokoa. Ni lazima mwendelee kuuamini. Ikiwa mtaacha, kuamini kwenu ni bure. Niliwapa ujumbe nilioupokea. Niliwaambia ukweli muhimu zaidi ya kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama Maandiko yanavyosema; kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama Maandiko yanavyosema na kwamba alimtokea Petro kisha mitume kumi na wawili. Baada ya hilo, aliwatokea waamini wengine zaidi ya mia tano kwa wakati mmoja. Wengi wao bado wanaishi sasa, lakini wengine wamekwisha kufa. Kisha alimtokea Yakobo na baadaye aliwatokea mitume wote. Mwisho wa yote kabisa alinitokea mimi. Nilikuwa tofauti, kama mtoto anayezaliwa wakati usiostahili. Mitume wengine wote ni wakuu kuliko mimi. Ninasema hivi kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu. Ndiyo sababu sistahili hata kuitwa mtume. Lakini, kwa sababu ya neema ya Mungu, ndivyo hivi nilivyo. Na neema aliyonipa haikupotea bure bila manufaa. Nilifanya kazi kwa bidii kuliko mitume wengine wote. (Lakini, kwa hakika si mimi niliyekuwa nafanya kazi. Ni neema ya Mungu iliyo ndani yangu.) Hivyo basi, si muhimu ikiwa ni mimi au mitume wengine ndiyo waliowahubiri, sisi sote tunawahubiri watu ujumbe huo huo, na hiki ndicho mlichoamini. Tunamwambia kila mtu kuwa Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Hivyo kwa nini baadhi yenu mnasema watu hawatafufuliwa kutoka kwa wafu? Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, basi Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu. Na ikiwa Kristo hakufufuliwa, ujumbe tunaowahubiri ni bure. Na imani yenu ni bure. Nasi tutakuwa na hatia ya kutoa ushuhuda wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumewahubiri watu kuhusu Yeye, kwa kusema kuwa alimfufua Kristo kutoka kwa wafu. Na ikiwa hakuna anayefufuliwa kutoka kwa wafu, basi Mungu hakumfufua Kristo. Ikiwa wale waliokufa hawatafufuliwa, basi Kristo hakufufuliwa pia. Na ikiwa Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu, basi imani yenu ni bure; bado mngali watumwa wa dhambi zenu. Na watu wa Kristo waliokwisha kufa wamepotea. Ikiwa tumaini letu katika Kristo ni kwa ajili tu ya maisha haya hapa duniani, basi watu watuhurumie sisi kuliko mtu mwingine yeyote. Lakini hakika Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu; ndiye wa kwanza miongoni mwa wafu wote watakaofufuliwa. Kifo huja kwa watu kwa sababu ya tendo la mtu mmoja. Lakini sasa kuna ufufuo kutoka kwa wafu kwa sababu ya mtu mwingine. Ndiyo, kwa sababu sisi sote ni wa Adamu, sisi sote tunakufa. Kwa njia hiyo hiyo, sisi sote tulio wa Kristo, tutakuwa hai tena. Lakini kila mmoja atafufuliwa kwa mpango sahihi. Kristo alikuwa wa kwanza kufufuliwa. Kisha atakaporudi, wale walio wake watafufuliwa. Ndipo mwisho utakuja. Kristo atamwangamiza kila mtawala na kila mamlaka na nguvu. Kisha atampa Mungu Baba ufalme. Kristo lazima atawale mpaka Mungu atakapowaweka adui zake wote chini ya udhibiti wake. Adui wa mwisho kuangamizwa ni kifo. Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu ameweka kila kitu chini ya udhibiti wake.” Inaposema “kila kitu” kimewekwa chini yake, hii ni wazi Mungu peke yake ndiye ambaye hayuko chini yake. Mungu ndiye anayeweka kila kitu chini ya udhibiti wa Kristo. Baada ya kuweka kila kitu chini ya Kristo, ndipo yeye mwenyewe, kama Mwana, atawekwa chini ya Mungu. Katika namna hii Mungu atakuwa mtawala mkuu juu ya kila kitu. Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, sasa watu wanafikiri wanafanya nini kwa kubatizwa kwa ajili ya wale waliokufa? Ikiwa wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini watu wanabatizwa kwa ajili yao? Na vipi kuhusu sisi? Kwa nini tunajiweka katika hatari wakati wote? Ninakumbana na kifo kila siku. Ni kweli, ndugu zangu kwamba ninajivuna kwa sababu ninyi ni wa Kristo Yesu Bwana wetu. Niliwapiga wanyama wa porini kule Efeso. Ikiwa nilifanya hivyo kwa sababu za kibinadamu tu, sijapata kitu. Ikiwa hatufufuliwi kutoka kwa wafu, “basi tule na tunywe, kwa sababu tutakufa kesho.” Msidanganywe: “Marafiki wabaya huharibu tabia njema.” Rudieni kuwaza kwenu kwa usahihi na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hamumjui Mungu. Ninasema hivi ili niwafedheheshe. Lakini mtu mmoja anaweza kuuliza, “Waliokufa wanafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” Haya ni maswali ya kijinga. Unapopanda kitu fulani, ni lazima kife udongoni kabla hakijawa hai na kuota. Na unapopanda kitu fulani, unachopanda hakina “mwili” sawa na ule kitakachokuwa nao baadaye. Unapanda mbegu, pengine ngano au kitu kingine. Na yeye Mungu hutoa mwili kwa kila aina ya mbegu. Vitu vyote vilivyoumbwa kwa mwili haviko sawa: Wanadamu wana aina moja ya mwili, wanyama wana aina nyingine, ndege wana nyingine na samaki nao wana aina yao. Pia kuna miili ya kimbingu na miili ya kidunia. Lakini uzuri wa miili ya kimbingu ni wa aina yake na uzuri wa miili ya kidunia ni kitu kingine. Jua lina uzuri wa aina yake, mwezi una aina yake na nyota zina aina nyingine ya uzuri. Na kila nyota iko tofauti kwa uzuri wake. Ndivyo itakavyokuwa waliokufa watakapofufuliwa na kuwa hai. Mwili “uliopandwa” kaburini utaharibika na kuoza, lakini utafufuliwa katika uhai usioharibika. Mwili hauna heshima “unapopandwa”. Lakini utakapofufuliwa, utakuwa na utukufu. Mwili unakuwa dhaifu “unapopandwa”. Lakini unapofufuliwa, unakuwa na nguvu nyingi. Mwili unaopandwa ni mwili wa kawaida, wa asili. Utakapofufuliwa utakuwa mwili wa ajabu uliopewa uwezo na Roho. Kuna mwili wa asili unaoonekana kwa macho. Na hivyo kuna mwili wa Kiroho wa ajabu. Kama Maandiko yanavyosema, “Mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe asili kilichokuwa hai.” Lakini Adamu wa mwisho akafanyika roho. Mtu wa kiroho hakuja kwanza. Mtu wa asili anayeonekana kwa macho ndiye alikuja kwanza; kisha akaja wa kiroho. Mtu wa kwanza alitokana na mavumbi ya dunia. Mtu wa pili alitoka mbinguni. Watu wote ni wa dunia. Wako sawa na yule mtu wa kwanza wa dunia. Lakini wale walio wa mbinguni wako kama mtu wa mbinguni. Tumeivaa sura ya mtu aliyetoka mavumbini, pia tutaivaa sura ya mtu aliyetoka mbinguni. Ninawaambia hili ndugu zangu: Miili yetu na nyama na damu haiwezi kuwa na nafasi katika ufalme wa Mungu. Kitu kitakachoharibika hakiwezi kuwa na sehemu katika kitu kisichoharibika kamwe. Lakini sikilizeni, ninawaambia siri hii: Sote hatutakufa, lakini sote tutabadilishwa. Itachukuwa sekunde moja. Tutabadilishwa kufumba na kufumbua. Hili litatokea parapanda ya mwisho itakapopulizwa. Parapanda itakapolia wale waliokufa watafufuliwa ili waishi milele. Na tutabadilishwa sote. Mungu ataibadilisha miili yetu ili isiharibike kamwe. Mwili huu unaokufa utabadilishwa na kuwa mwili usiokufa. Hivyo mwili huu unaokufa utajivika kutokufa. Hili litakapotokea, ndipo Maandiko yatatimilizwa: “Mauti imemezwa katika ushindi. Ewe kifo, ushindi wako uko wapi? Nguvu yako ya kudhuru iko wapi?” Dhambi ni nguvu ya mauti inayodhuru, na nguvu ya dhambi ni sheria. Lakini tunamshukuru Mungu anayetupa ushindi kupitia Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo, kaka na dada zangu, simameni imara. Msiruhusu kitu chohote kiwabadilishe. Jitoeni nafsi zenu kikamilifu kwa kazi yenu katika Bwana. Mnajua ya kuwa chochote mnachofanya kwa ajili ya Bwana hakitapotea bure bila manufaa. Sasa, kuhusu mchango wa pesa kwa ajili ya watu wa Mungu: Fanyeni kama nilivyoyaambia makanisa ya Galatia kufanya. Siku ya kwanza ya kila wiki, kila mmoja wenu achukue kiasi cha pesa kutoka kwenye pesa zake na azitenge. Akusanye kiasi anachoweza kutokana na anavyobarikiwa. Na hivyo hamtahitaji kukusanya nitakapokuja. Nitakapofika, nitatuma baadhi ya watu wapeleke sadaka yenu Yerusalemu. Hawa watakuwa wale ambao ninyi mtakubali kuwa waende. Nitawatuma na barua ya utambulisho. Ikiwa itakuwa vizuri kwangu kwenda pia, basi tutasafiri pamoja. Nimepanga kupitia Makedonia, hivyo nitakuja kwenu baada ya hapo. Pengine nitakaa kwenu kwa muda. Pengine nitakaa kwenu majira yote ya baridi. Hivyo mtaweza kunisaidia katika safari yangu, kila ninapokwenda. Sitaki kuja kuwaona sasa, kwa sababu nitaweza tu kukaa nanyi kwa muda mfupi, kabla haijanilazimu kwenda mahali pengine. Ninategemea kukaa pamoja nanyi kwa muda mrefu, ikiwa Bwana ataruhusu. Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste. Nitakaa hapa, kwa sababu sasa nimepewa fursa nzuri kwa kazi kubwa na inayokua. Na kuna watu wengi wanaopinga. Timotheo atakapokuja kwenu, mjitahidi akae kwa raha na amani akiwa kwenu. Anafanya kazi kwa ajili ya Bwana kama mimi. Hivyo yeyote miongoni mwenu asikatae kumpokea Timotheo. Msaidieni aendelee katika safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu. Ninategemea atakuja kwangu pamoja na ndugu wengine. Na sasa kuhusu Apolo: Ninamsihi sana aje na ndugu wengine kuwatembelea ninyi huko Korintho. Hajataka kuja sasa, lakini atakuja kwenu atakapopata nafasi. Iweni waangalifu. Simameni imara katika imani yenu. Mwe jasiri na wenye nguvu. Fanyeni kila kitu katika upendo. Mnajua kuwa Stefana na familia yake walikuwa waamini wa kwanza katika Akaya. Wamejitia katika kazi ya kuwahudumia watu wa Mungu. Ndugu zangu, ninawaomba, mjiweke chini ya uongozi wa watu kama hawa na wengine wanaofanya kazi kwa bidii na kutumika pamoja nao. Ninafurahi kwa sababu Stefana, Fortunato na Akaiko wamekuja. Hamko hapa pamoja nami lakini wamejaza nafasi yenu. Wamekuwa faraja kuu kwangu na kwenu pia. Basi, mnapaswa kuitambua thamani ya watu kama hawa. Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Priska wanawasalimu katika Bwana. Na kanisa linalokutana nyumbani mwao linawasalimu pia. Ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kila mmoja wenu kwa salamu maalum ya watu wa Mungu. Hii ni salamu yangu kwa mkono wangu mwenyewe: PAULO. Ikiwa mtu yeyote hampendi Bwana, mwacheni mtu huyo abaki chini ya laana ya Mungu. Njoo, Ewe Bwana! Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja nanyi. Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu. Salamu kutoka kwa Paulo, Mtume wa Kristo Yesu. Mimi ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alitaka. Na Timotheo ndugu yetu katika Kristo. Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho na kwa watakatifu wote wa Mungu walio jimbo lote la Akaya. Neema na Amani iwe kwenu kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo. Sifa na zimwendee Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni baba aliyejaa rehema, Mungu aliye mwingi wa faraja. Hutufariji kila wakati tunapokuwa katika hali ya matatizo ili wengine wawapo katika matatizo, tuweze kuwafariji kwa namna ile ile ambayo Mungu ametufariji sisi. Twashiriki katika mateso mengi ya Kristo. Na kwa namna hiyo hiyo, faraja nyingi hutujia kwa njia ya Kristo. Ikiwa tuko katika mateso, tuko kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu. Na ikiwa tunafarijika, ni kwa sababu tuweze kuwafariji ninyi. Hili huwasaidia katika kuyakubali mateso yale yale tunayopata kwa uvumilivu. Tumaini letu kwenu liko imara. Tunafahamu kuwa mnashiriki katika mateso yetu. Hivyo tunafahamu pia kuwa mnashiriki katika faraja yetu pia. Ndugu zangu, tunapenda mfahamu juu ya mateso tuliyoyapata hapa Asia. Tulikuwa na mzigo sana huko, ulikuwa mzito kuliko hata nguvu zetu. Hata tulipoteza tumaini la kuishi. Ukweli ni kuwa, ilionekana kana kwamba Mungu alikuwa anatuambia kuwa tunakwenda kufa. Lakini haya yalitokea ili tusizitumainie nguvu zetu bali tumtumainie Mungu, ambaye huwainua watu toka mautini. Yeye alituokoa toka katika hatari hizi kubwa za mauti, na ataendelea kutuokoa. Twajisikia kuwa na hakika kuwa ataendelea kutuokoa. Nanyi mnaweza kutusaidia kwa njia ya maombi. Ndipo watu wengi wataweza kumshukuru Mungu kwa ajili yetu; kwamba Mungu alitubariki kutokana na maombi yao mengi. Hili ndilo tunalojivunia, na naweza kusema kwa dhamiri safi kwamba ni kweli: Katika kila kitu tulichofanya duniani, Mungu ametuwezesha kukifanya kwa moyo safi. Na hili ni kweli zaidi katika yale tuliyowatendea ninyi. Tulifanya hivyo kwa neema ya Mungu, si kwa hekima ambayo ulimwengu unayo. Tunawaandikia mambo mnayoweza kusoma na kuyaelewa. Na nina matumaini kuwa mtayaelewa inavyopasa kama ambavyo tayari mmekwisha kuyafahamu mambo mengi kuhusu sisi. Natumaini mtaelewa kuwa mnaweza kuona fahari juu yetu, kama nasi tutakavyoona fahari juu yenu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja. Nilikuwa na uhakika sana juu ya haya yote. Ndiyo maana niliweka mpango wa kuwatembelea kwanza. Kisha mngebarakikwa mara mbili. Nilipanga kuwatembelea nilipokuwa nikienda Makedonia na nilipokuwa ninarudi. Na nilipanga kuwaomba mniletee kutoka huko hadi Yudea chochote ambacho nilihitaji kwa ajili ya safari yangu. Je! Mnadhani nilipanga mipango hii bila kufikiri? Au mnadhani ninafanya mipango kama vile dunia inavyofanya, lugha yetu kwenu si ndiyo na hapana kwa wakati mmoja. Kama ambavyo kwa hakika mnaweza kumwamini Mungu, basi mnaweza kuamini kuwa lile tunalowaambia kamwe haliwezi kuwa ndiyo na hapana kwa pamoja. Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, Yeye ambaye Sila, Timotheo, na mimi tuliwaeleza habari zake, hakutokea kuwa ni ndiyo na hapana kwa ahadi za Mungu. Kinyume chake ndiyo ya Mungu imethibitika daima katika Kristo kuwa ni ndiyo. Ndiyo kwa ahadi zote za Mungu katika Kristo. Na hii ndiyo maana twasema “Amina” Katika Kristo kwa utukufu wa Mungu. Na Mungu ndiye anayewafanya ninyi na sisi kuwa imara katika Kristo. Mungu pia ndiye aliyetuchagua kwa ajili ya kazi yake. Aliweka alama yake juu yetu ili kuonesha kuwa tu mali yake. Ndiyo, amemweka roho wake ndani ya mioyo yetu kama malipo ya awali yanayotuhakikishia mambo yote atakayotupa. Ninawaambia hili, na ninamwomba Mungu awe shahidi wangu kuwa ni la kweli: Sababu iliyonifanya nisirudi tena Korintho ni kuwa nilitaka niepuke kuwapa karipio lenye nguvu. Sina maana ya kuwa tunataka kuitawala imani yenu. Ninyi mpo imara katika imani. Lakini tunatenda kazi pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu wenyewe. Hivyo niliamua moyoni mwangu mwenyewe kuwa sitafanya safari nyingine ya huzuni kuja kwenu. Ikiwa nitawafanya muwe na huzuni nani atanifanya niwe na furaha? Ni ninyi tu ndiyo mnaweza kunifanya niwe na furaha. Ni ninyi ambao niliwahuzunisha. Naliwaandikia barua ili kwamba nijapo kwenu nisihuzunishwe na wale ambao wanapaswa kunifanya niwe na furaha. Nilijisikia kuwa na hakika ya kuwa ninyi nyote mtashiriki furaha yangu. Nilipowaandikia barua ya kwanza, niliiandika macho yangu yakibubujika machozi mengi. Sikuandika ili kuwafanya muwe na huzuni, bali kuwafanya mjue kwa jinsi gani ninavyowapenda. Mtu mmoja katika kusanyiko lenu amesababisha maumivu, ila si kwangu, bali amesababisha maumivu kwenu nyote kwa kiwango fulani. Nina maanisha amewakwaza nyote kwa namna fulani. (Sitaki ionekane kuwa mbaya sana kuliko ilivyo) Adhabu ambayo walio wengi miongoni mwa kusanyiko lenu walimpa inatosha. Lakini msameheni na kumtia moyo sasa. Hili litamsaidia asiwe na huzuni sana na asikate tamaa kabisa. Hivyo ninawasihi mwonesheni kuwa mnampenda. Hii ndiyo sababu niliandika ile barua. Nilitaka kuwapima na kuona ikiwa mna utii katika kila kitu. Mkimsamehe mtu, ndipo nami husamehe pia. Na kile nilichosamehe, kama nilikuwa na jambo la kusamehe, nilisamehe kwa ajili yenu. Na Kristo akithibitisha. Nilifanya hivi ili Shetani asipate ushindi wowote kutoka kwetu. Tunafahamu sote mipango yake ilivyo. Nilikwenda Troa kuwaambia watu Habari Njema juu ya Kristo. Bwana alinipa fursa ya pekee kule. Lakini sikuwa na amani kwa sababu sikumwona Tito pale. Hivyo niliaga na kwenda Makedonia. Lakini ashukuriwe Mungu ambaye siku zote hutuongoza katika gwaride la ushindi la Kristo. Mungu anatutumia sisi kueneza ufahamu juu ya Kristo kila mahali kama vile marashi yanayonukia vizuri. Maisha yetu ni sadaka ya harufu nzuri ya manukato ya Kristo inayotolewa kwa Mungu. Harufu nzuri ya sadaka hii huwaendea wale wanaokolewa na kwa wale wanaopotea. Kwao wanaopotea, marashi haya yananukia kama mauti, na huwaletea kifo. Ila kwao wanaookolewa, ina harufu nzuri ya uzima, na inawaletea afya ya uzima. Kwa hiyo ni nani aliye bora kuifanya kazi hii? Kwa hakika sio wale wanaozunguka wakiuuza ujumbe wa Mungu ili kupata faida! Lakini sisi hatufanyi hivyo. Kwa msaada wa Kristo tunaisema kweli ya Mungu kwa uaminifu, tukifahamu kuwa tunazungumza kwa ajili yake na mbele zake. Je, mnadhani tunaanza kujitafutia sifa? Je, tunahitaji barua za utambulisho kuja kwenu au kutoka kwenu kama wengine? Hapana, ninyi wenyewe ni barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu. Inafahamika na kusomwa na watu wote. Mnaonyesha kuwa ninyi ni barua toka kwa Kristo aliyoituma kupitia sisi. Barua ambayo haikuandikwa kwa wino bali kwa Roho wa Mungu aliye hai. Haikuandikwa katika mbao za mawe lakini katika mioyo ya wanadamu. Tunaweza kusema hili, kwa sababu Kristo ndiye anayetupa uhakika huu mbele za Mungu. Simaanishi kuwa tuna uwezo wa kufanya jambo lolote jema kwa uwezo wetu wenyewe. Mungu ndiye anatuwezesha kufanya yote tunayoyafanya. Ametuwezesha pia kuwa watumishi wa agano jipya lililotoka kwake kwenda kwa watu wake. Si agano la sheria zilizoandikwa, ni la Roho. Sheria zilizoandikwa huleta mauti, bali Roho huleta uzima. Agano la kale lililoleta mauti, lililoandikwa kwenye mawe, lilikuja na utukufu wa Mungu. Kwa kweli, uso wa Musa ulikuwa unang'aa utukufu (Utukufu uliokuwa na ukomo) hata watu wa Israel hawakuweza kuendelea kumtazama usoni. Hivyo kwa hakika zaidi huduma ya agano jipya linalokuja kutoka kwa Roho anayeleta uzima lina utukufu zaidi. Maana yangu ni kuwa: utaratibu wa zamani wa kumtumikia Mungu uliwaweka watu katika hatia ya dhambi na kuwapa hukumu, lakini lilikuwa na utukufu. Hivyo kwa hakika utaratibu mpya wa kumtumikia Mungu unaowaweka huru watu kutoka hukumu una utukufu mkubwa zaidi. Utaratibu wa zamani wa utumishi kwa Mungu ulikuwa na utukufu. Lakini kwa hakika unapoteza utukufu wake unapolinganishwa na utukufu mkubwa zaidi wa utaratibu mpya wa utumishi kwa Mungu. Ikiwa utumishi ule wa muda ulikuja na utukufu, basi utumishi wa kudumu umekuja na utukufu mkubwa zaidi. Kwa sababu tuna tumaini hili tunatenda kwa ujasiri mkubwa. Hatuko kama Musa, ambaye alifunika uso wake ili watu wa Israel wasiendelee kuona kuwa utaratibu wa zamani wa kumtumikia Mungu ulikuwa unaelekea mwisho. Lakini mioyo yao ilikuwa imefungwa. Na hata leo, watu wale wanapolisoma agano la kale, fahamu zao zinakuwa zimefunikwa. Ni kwa kupitia Yesu Kristo tu agano la kale linaondolewa. Ndiyo, hata leo, wanaposoma sheria ya Musa, fahamu zao zimefunikwa. Lakini, kama maandiko yanavyosema juu ya Musa, “Kila anapomgeukia Bwana, ufahamu wake unafunuliwa.” Katika maandiko hayo Bwana ni Roho, na palipo na Roho wa Bwana, pana uhuru. Na sura zetu hazikufunikwa. Sote tunaendelea kuutazama utukufu wa Bwana, na tunabadilishwa na kufanana na mfano huo huo tunaouona. Badiliko hili linatuletea utukufu zaidi na zaidi, na linatoka kwa Bwana, ambaye ni Roho. Mungu, kwa rehema zake, alitupa sisi huduma hii ili tuifanye, hivyo hatukati tamaa. Lakini tumekataa mambo ya aibu ya siri. Hatumdanganyi mtu yeyote, na hatuyabadilii mafundisho ya Mungu. Tunaifundisha kweli wazi wazi. Na hivi ndivyo watu wanaweza kutambua mioyoni mwao sisi ni watu wa namna gani mbele za Mungu. Habari Njema tunazowahubiri watu hazijafichika kwa yeyote isipokuwa kwa waliopotea. Mtawala wa dunia hii amezitia giza akili za wasioamini. Hawawezi kuona nuru ya Habari Njema; ujumbe juu ya uungu wa Kristo, taswira halisi ya Mungu. Hatuwaambii watu habari zetu wenyewe. Lakini tunawaambia habari za Kristo Yesu kuwa ni Bwana, na tunawaambia kuwa sisi ni watumwa wenu kwa ajili ya Yesu. Kuna wakati Mungu alisema, “Na nuru ing'ae gizani” na huyu ni Mungu yule yule anayesababisha nuru ing'ae katika mioyo yetu ili tutambue utukufu wa uungu wake mkuu unaongaa katika sura ya Kristo. Tuna hazina hii kutoka kwa Mungu, lakini sisi ni kama vyombo vya udongo tu vinavyobeba hazina. Hii ni kuonesha kuwa nguvu ya kustaajabisha tuliyo nayo inatoka kwa Mungu, si kwetu. Tunasumbuliwa kila upande, lakini hatushindwi. Mara kwa mara hatujui tufanye nini, lakini hatukati tamaa. Tunateswa, lakini Mungu hatuachi. Tunaangushwa chini wa nyakati zingine, laki hatuangamizwi. Hivyo tunashiriki kifo cha Yesu katika miili yetu kila wakati, lakini haya yanatokea ili uzima wa Yesu udhihirishwe katika miili yetu. Tuko hai, lakini kwa ajili ya Yesu tupo katika hatari ya kifo kila wakati, ili kwamba uzima wa Yesu udhihirishwe katika miili yetu ya kufa. Kwa hiyo kifo kinafanya kazi ndani yetu, lakini matokeo yake ni kwamba uzima unafanya kazi ndani yenu. Maandiko yanasema, “Niliamini, hivyo nikasema.” Tuna Roho huyo huyo anayetupa imani kama hiyo. Tunaamini, na hivyo tunasema pia. Mungu alimfufua Bwana Yesu kutoka kwa wafu, nasi tunajua kuwa atatufufua pamoja na Yesu. Mungu atatukusanya pamoja nanyi, na tutasimama mbele zake. Mambo yote haya ni kwa ajili yenu. Na hivyo neema ya Mungu inatolewa kwa watu wengi zaidi na zaidi. Hili litaleta shukrani nyingi zaidi na utukufu kwa Mungu. Hii ndiyo sababu hatukati tamaa. Miili yetu inazidi kuzeeka na kuchoka, lakini roho zetu ndani zinafanywa upya kila siku. Tuna masumbufu, lakini ni madogo na ni ya muda mfupi. Na masumbufu haya yanatusaidia kuupata utukufu wa milele ulio mkuu kuliko masumbufu yetu. Hivyo twafikiri juu ya mambo tusiyoweza kuyaona, si tunayoona. Tunayoyaona ni ya kitambo tu, na yale tusiyoyaona yanadumu milele. Tunafahamu kuwa miili yetu, ambayo ni hema tunaloishi ndani yake hapa duniani itaharibiwa. Hilo litakapotokea, Mungu atakuwa na nyumba tayari kwa ajili yetu kuishi ndani yake. Haitakuwa nyumba kama ambayo watu hujenga hapa duniani. Itakuwa nyumba ya mbinguni itakayodumu milele. Lakini wakati bado tunaishi katika miili hii, tunaugua kwa sababu tuna shauku kubwa mbele za Mungu ya kutupa mwili wetu mpya wa mbinguni ili tuweze kujivika. Tutauvaa mwili wa mbinguni kama vazi jipya na hatutakuwa uchi. Tunapoishi katika “hema” hili la kidunia, tunaugua na kuelemewa na mizigo. Lakini, hiyo si kwa sababu tunataka kuivua miili hii ya zamani. Hapana, ni kwa sababu tunataka kuivaa miili yetu mipya. Kisha mwili huu unao kufa utafunikwa na uzima. Hii ndiyo sababu Mungu mwenyewe ndiye aliyetuandaa kwa kusudi hili hasa. Na ametupata Roho kama malipo ya awali kutuhakikishia maisha yajayo. Hivyo tuna ujasiri daima. Tunafahamu kuwa tunapoendelea kuishi katika mwili huu, tunakuwa mbali na makao yetu pamoja na Bwana. Tunaishi kwa msingi wa yale tunayoamini kuwa yatatokea na siyo kwa msingi wa yale tunayoyaona. Hivyo ninasema tuna ujasiri. Na tungependa kuondoka na kutokuwa katika mwili huu na kuwa nyumbani pamoja na Bwana. Lengo letu pekee ni kumpendeza Bwana, kwamba tupo nyumbani au mbali. Tutasimama sote mbele za Kristo ili tuhukumiwe. Kila mtu atalipwa anachostahili. Kila mtu atalipwa kutokana na matendo yake, mazuri au mabaya, alipoishi katika mwili huu wa kidunia. Tunafahamu maana ya kuwa na hofu na Bwana, hivyo tunajitahidi kuwashawishi watu waipokee. Mungu anafahamu tulivyo, na ni matarajio yangu kuwa nanyi mioyoni mwenu mnatufahamu sisi pia. Hatujaribu tena kujithibitisha kwenu sasa. Lakini tunawapa sababu za ninyi kujivuna kwa ajili yetu. Kisha mtaweza kuwa na majibu kwa ajili wanaojivuna kwa ajili ya yale yanayoonekana. Hawajali kuhusu kilicho katika moyo wa mtu. Ikiwa tuna wazimu, ni kwa ajili ya Mungu na ikiwa tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu. Upendo wa Kristo unatutawala, kwa sababu tunafahamu kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote. Hivyo wote wamekufa. Alikufa kwa ajili ya wote ili wanaoishi wasiendelee kuishi kwa ajili yao wenyewe. Alikufa kwa ajili yao na alifufuka toka kwa wafu ili waishi kwa ajili yake. Kuanzia sasa hatumfikirii mtu yeyote kama ulimwengu unavyowafikiria watu. Ni kweli kuwa zamani kale tulimfikiria Kristo kwa mtazamo wa kidunia. Lakini hatufikirii hivyo sasa. Mtu anapokuwa ndani ya Kristo, anakuwa kiumbe kipya kabisa. Mambo ya zamani yanakoma; na ghafla kila kitu kinakuwa kipya! Yote haya yatoka kwa Mungu. Kupitia Kristo, Mungu alifanya amani katika yake na sisi. Na Mungu alitupa kazi ya kuleta amani kati ya watu na Mungu. Tunachosema ni kuwa kupitia Kristo, Mungu alikuwa anaweka amani kati yake na ulimwengu. Alikuwa anatoa ujumbe wa msamaha kwa kila mtu kwa matendo mabaya waliyotenda kinyume naye. Na alitupa ujumbe huu wa amani ili kuwaeleza watu. Hivyo tumetumwa kwa ajili ya Kristo. Ni kama Mungu anawaita watu kupitia sisi. Tunazungumza kwa niaba ya Kristo tunapowasihi ninyi kuwa na amani na Mungu. Kristo hakuwa na dhambi, ila Mungu alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu ili ndani ya Kristo tuweze kufanyika kielelezo cha wema wa uaminifu wa Mungu. Sisi ni watenda kazi pamoja na Mungu. Hivyo tunawasihi: Neema mliyoipokea kutoka kwa Mungu iwe na manufaa kwenu. Mungu anasema, “Nilikusikia kwa wakati sahihi, na nikakusaidia siku ya wokovu.” Ninawaambia kwamba “wakati uliokubalika” ni huu sasa. Na “Siku ya wokovu” ni leo. Hatutaki watu waone makosa katika kazi yetu. Hivyo hatutendi jambo lolote litakalokuwa kikwazo kwa wengine. Lakini kwa kila njia tunaonesha kuwa sisi ni watumishi wa Mungu. Hatukati tamaa, ingawa tunakutana na matatizo, mambo magumu na matatizo ya kila namna. Tumepigwa na kutupwa gerezani. Watu wameanzisha fujo dhidi yetu. Tumefanya kazi kwa bidii, mara nyingi pasipo kula ama kulala. Tunadhihirisha kuwa sisi tu watumishi wa Mungu kutokana na maisha yetu safi, kwa ufahamu wetu, kwa subira yetu na kwa upole wetu. Tunadhihirisha hilo kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo wetu wa kweli, kwa kusema iliyo kweli, na kwa kuzitegemea nguvu za Mungu. Njia hii iliyo sahihi ya kuishi imetuandaa kujitetea wenyewe kinyume na kila aina ya shambulizi. Baadhi ya watu wanatuheshimu, lakini wengine wanatudhihaki. Wengine wanasema mema juu yetu, lakini wengine wasema mabaya juu yetu. Wengine wanatusema kuwa tu waongo, lakini tunasema kweli. Kwa wengine hatufahamiki, lakini twajulikana sana. Tunaonekana kama watu wanaostahili kufa, lakini angalia! Twadumu kuishi. Tunaadhibiwa, lakini hatuuawi. Tuna huzuni nyingi, lakini tunafuraha kila siku. Tu maskini, lakini tunawafanya watu wengi kuwa matajiri katika imani. Hatuna kitu, lakini tunakila kitu. Tumesema kwa uhuru kwenu ninyi watu wa Korintho. Tumefungua mioyo yetu kwenu. Upendo wetu kwenu haujakoma. Ninyi ndiyo mliouzuia upendo wenu kwetu. Ninawaambia kama watoto wangu. Fanyeni vivyo hivyo kama sisi tulivyotenda kwenu; fungueni mioyo yenu pia. Ninyi hamko sawa na wale wasioamini. Hivyo msifungwe nira pamoja nao. Wema na ubaya havikai pamoja. Nuru na giza haviwezi kukaa pamoja katika chumba kimoja. Itawezekanaje kuwe na mapatano kati ya Kristo na beliali? Je, mwamini anashirika gani na asiye amini? Hekalu la Mungu halina mapatano yoyote na sanamu, na sisi tu hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu anavyosema, “Nitakaa kati yao na kutembea nao; Nitakuwa Mungu wao, na watakuwa watu wangu.” “Hivyo tokeni nje kati yao na jitengeni nao, asema Bwana. Msishike chochote kilicho kichafu, nami nitawakaribisha.” “Nitakuwa baba yenu, nanyi mtakuwa wana wangu na binti zangu, asema Bwana Mwenyezi.” Rafiki wapendwa, tuna ahadi hizi toka kwa Mungu. Hivyo tujitakase maisha yetu na kuwa huru kutoka kwa kila kinachofanya miili yetu ama roho zetu kuwa najisi. Heshima yetu kwa Mungu itufanye tujaribu kuwa watakatifu kabisa kwa namna tunavyoishi. Fungueni mioyo yenu kwetu. Hatujamtendea vibaya wala kumwumiza mtu yeyote. Na hatujamdanganya mtu yeyote. Sisemi haya kuwalaumu. Nimekwishawaeleza kuwa tunawapenda sana kiasi kwamba hakuna chochote katika maisha ama katika kifo kitakachotutenganisha na ninyi. Ninajisikia kwamba ninaweza kuwaambia lolote. Ninajivunia sana ninyi. Licha ya matatizo yote tuliyoyapata, nimetiwa moyo sana na ninajisikia kuwa mwenye furaha sana. Tulipokuja Makedonia, hatukupumzika. Tulisumbuliwa kwa kila namna. Tulikuwa na vita kwa nje na hofu ndani yetu. Lakini Mungu huwapa moyo wale wanaosumbuliwa, na kwa hakika na sisi alitupa moyo kwa kumleta Tito kwetu. Ilikuwa furaha kumwona, lakini tulitiwa moyo zaidi tuliposikia jinsi nanyi mlivyomtia moyo yeye pia. Naye alitueleza kuwa mlikuwa na shauku ya kuniona mimi na kwamba mnayajutia yale mlivyofanya. Na akatueleza jinsi mlivyokuwa na shauku ya kusimama upande wangu. Niliposikia hili, nilifurahishwa sana. Hata kama barua nilyowaandikieni iliwahuzunisha, sijutii kuiandika. Nafahamu kuwa barua ile iliwatia huzuni, ninasikitika kwa hilo. Lakini iliwapa huzuni kwa muda mfupi. Sasa ninafurahi, si kwa sababu mlipata huzuni, bali kwa sababu huzuni yenu iliwasababisha mkaamua kubadilika. Hilo ndilo ambalo Mungu alilitaka, hivyo hatukuwaumiza kwa namna yo yote. Aina ya huzuni ambayo Mungu anaitaka inawafanya watu waamue kubadili maisha yao. Hili linawaelekeza kwenye wokovu, nasi hatuwezi kulijutia hilo. Lakini huzuni dunia huleta mauti. Mlikuwa na huzuni ambayo Mungu alitaka muwe nayo. Sasa mmetambua kile ambacho huzuni hiyo imewaletea: Imewafanya muwe makini sana. Imewafanya mtafute kuthibitisha kuwa hamkufanya makosa. Iliwafanya mkasirike na mwogope. Imewafanya muwe na shauku ya kuniona. Imewafanya muwe na azma ya kufanya kile nilichowaagiza. Imewafanya muwe na shauku ya kuona kuwa haki inatendeka. Mlithibitisha kuwa hamkuwa na hatia katika sehemu yoyote ya tatizo hilo. Sababu kubwa ya kuandika barua ile haikuwa kwa sababu ya yule aliyefanya kosa au aliyeumia. Niliandika ili mtambue, mbele za Mungu, jinsi mnavyotujali sana sisi. Na hili ndilo lililokuwa faraja kwetu sisi. Tulitiwa moyo sana, lakini hasa tulifurahishwa kuona jinsi Tito alivyokuwa mwenye furaha. Ninyi nyote mlimfanya apate utulivu moyoni. Nilijisifu juu yenu kwake Tito, na ninyi hamkuniaibisha. Siku zote tumewaambia ninyi kweli, na sasa yale tuliyomwambia Tito kwa habari zenu yamedhihirika kuwa ni kweli. Na upendo wake kwenu una nguvu anapokumbuka kuwa mlikuwa tayari kutii. Mlimpokea kwa heshima na hofu. Ninafuraha sana kwa kuwa ninaweza kuwaamini kikamilifu. Na sasa, kaka na Dada zetu, tunataka kuwaambia kile ambacho neema ya Mungu imefanya katika makanisa ya makedonia. Waamini hawa wamepitia katika masumbufu makubwa, na ni maskini sana. Lakini furaha yao kubwa iliwafanya kuwa wakarimu zaidi katika kutoa kwao. Ninaweza kuwaambia kwamba walitoa kulingana na uwezo wao na hata zaidi ya uwezo wao. Hakuna mtu yeyote aliyewaambia kufanya hivyo. Hilo lilikuwa wazo lao. Walituuliza tena na tena na walitusihi tuwaruhusu kushiriki katika huduma hii kwa ajili ya watu wa Mungu. Na walitoa kwa namna ambayo sisi wenyewe hatukutegemea: kwanza walijitoa wenyewe kwa Mungu na kwetu kabla ya kutoa fedha zao. Hili ndilo Mungu anataka. Kwa hiyo tulimwomba Tito awasaidie ninyi kuikamilisha kazi hii maalum ya kutoa. Tito ndiye aliyeianzisha kazi hii kwanza miongoni mwenu. Ninyi ni matajiri kwa kila kitu; katika imani, katika uwezo wa kuzungumza, katika maarifa, katika utayari wa kusaidia kwa njia yo yote, na katika upendo mliojifunza kutoka kwetu. Hivyo sasa tunawataka muwe matajiri katika kazi hii ya kutoa pia. Siwashurutishi ninyi kutoa, ila nataka niujaribu upendo wenu kuona ni wa kiasi gani kuwalinganisha na wengine ambao wamekuwa tayari na wana hiari ya kusaidia. Mnaifahamu neema ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mnafahamu kuwa aliacha utajiri wake mbinguni na kufanyika maskini kwa ajili yenu. Aliacha kila kitu ili ninyi mbarikiwe kwa wingi zaidi. Hili ndilo ninafikiri mnapaswa kufanya: mwaka jana mlikuwa wa kwanza kutaka kutoa, na mkawa wa kwanza kutoa. Hivyo sasa ikamilisheni kazi mliyoianzisha. Kisha kutenda kwenu kutakuwa sawa na “kutaka” kwenu “kutenda”. Toeni kutokana na kile mlicho nacho. Ikiwa mnataka kutoa, sadaka yenu itapokelewa. Sadaka yenu itahukumiwa kutokana na kile mlicho nacho, si kwa kile msichonacho. Hatupendi muwe na mizigo wakati wengine wanastarehe. Tunataka kila kitu kiwe katika hali ya usawa. Wakati huu mnavyo vingi na kuzidi na mnaweza kuwapa kila wanachohitaji. Kisha baadaye, watakapokuwa navyo vingi, wataweza kuwapa mnavyohitaji. Kisha kila mmoja atakuwa na mgao ulio sawa. Kama Maandiko yanavyosema, “Wale waliokusanya vingi hawakuwa na vingi zaidi, na wale waliokusanya kidogo hawakuwa na vichache zaidi.” Namshukuru Mungu kwa sababu alimpa Tito upendo ule ule nilionao mimi kwenu. Tito alikubali kufanya vile tulivyomwomba. Yeye mwenyewe alitamani sana kuja kwenu. Tunamtuma Tito pamoja ndugu anayekubalika katika makanisa yote. Anasifiwa kwa sababu ya huduma yake ya Habari Njema. Pia, alichaguliwa na makanisa kuambatana nasi tunapoleta sadaka hii. Tunafanya huduma hii kumpa Bwana heshima na kuonesha kuwa tunapenda kusaidia. Tunajitahidi kuwa waangalifu ili asiwepo mtu wa kutukosoa kwa namna ambavyo tunashugulika na sadaka hii kubwa. Tunajaribu kutenda lililo jema. Tunataka kufanya kile ambacho Bwana anakubali kuwa sahihi na kile ambacho watu wanafikiri kuwa ni sahihi. Pia, tunawatuma pamoja nao kaka yetu ambaye yuko tayari siku zote kutoa msaada. Amethibitisha hili kwetu mara nyingi na kwa njia nyingi. Na anataka kusaidia zaidi sasa kwa sababu ana imani zaidi nanyi. Na sasa kuhusu Tito, yeye ni mshirika mwenzangu. Anafanya kazi pamoja nami kuwasaidia ninyi. Na kuhusu hawa kaka wawili wengine: wao wametumwa kutoka katika makanisa mengine, na wanaleta heshima kwa Kristo. Hivyo waonesheni watu hawa kuwa mna upendo. Waonesheni kwa nini tunajisifia ninyi. Ndipo makanisa yote yatakapo tambua hili. Kwa hakika sina haja ya kuwaandikia ninyi juu ya msaada huu kwa watu wa Mungu. Ninajua kuwa mnataka kusaidia. Nimekuwa ninajisifu sana juu yenu kwa watu wa Makedonia. Niliwaeleza kwamba ninyi watu wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana. Na shauku yenu ya kutoa zaidi imewafanya watu walio wengi zaidi hapa wawe tayari kutoa pia. Lakini ninawatuma kaka hawa kwenu. Sipendi kujisifia kwetu juu yenu kuthibitishwe kuwa ni batili. Nataka muwe tayari kama ambavyo nimesema kuwa mtakuwa tayari. Ikiwa baadhi ya Wamakedonia walio wengi wangefuatana nami na kuwakuta hamko tayari, tutaaibika. Tutaibika kwa kuwa tulikuwa na uhakika sana juu yenu. Na ninyi mtaaibika pia! Hivyo nikafikiri kuwa niwaombe ndugu hawa waje kwenu kabla ya mimi kuja. Wao watasaidia kufanya maandalizi mapema kwa ajili ya sadaka yenu yenye ukarimu mliyoahidi. Kisha sadaka hii itakuwa tayari tutakapokuja, na itaonekana kuwa baraka, na si kitu kidogo ambacho hamkutaka kutoa. Kumbukeni hili: Yeye apandaye mbegu chache atapata mavuno kidogo. Lakini apandaye kwa wingi atapata mavuno mengi. Kila mmoja wenu atoe kama alivyo kusudia kutoa katika moyo wake. Hampaswi kutoa ikiwa mnajisia huzuni kufanya hivyo au ikiwa mnasikia kulazimishwa kutoa. Mungu anawapenda wale wanaotoa kwa furaha. Na Mungu anaweza kuwapeni baraka zaidi kuliko mlivyo katika kuhitaji kwenu, na daima mtakuwa na kila kitu mnachokihitaji. Mtakuwa na vingi vya ziada vya kutoa kwa kila kazi njema. Kama Maandiko yanavyosema, “Hawakuwa na choyo waliwapa maskini. Mambo mema waliyoyafanya yatadumu millele.” Mungu ndiye huwapa mbegu wale wanaopanda, na anatoa mkate kuwa chakula. Na Mungu atawapeni “mbegu” na kuifanya ile mbegu ikue. Atazalisha mazao makubwa kutokana na wema wenu. Mungu atawatajirisha katika namna zote ili mweze kutoa kwa uhuru kila mara. Na kutoa kwenu kulikosimamiwa na sisi kutawafanya watu wamshukuru Mungu. Huduma mnayoitoa inawasaidia watu wa Mungu katika mahitaji yao, lakini si hayo tu itendayo. Inaleta pia shukrani nyingi zaidi na zaidi kwa Mungu. Huduma hii ni uthibitisho wa imani yenu, na watu watamsifu Mungu kwa sababu kwa uhuru mlitoa mkawapa sehemu pamoja na watu wengine pia. Watamsifu Mungu kwa sababu wanaona jinsi mnavyoifuata injili ya Yesu Kristo ambayo mliipokea kwa wazi kabisa. Na wanapoomba kwa ajili yenu, watatamani wangekuwa pamoja nanyi. Watajisikia hivi kwa sababu ya neema ya ajabu aliyowapa Mungu. Mungu apewe shukrani kwa kipawa chake ambacho ni ajabu sana kukielezea. Mimi, Paulo, ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo. Wengine wanasema kuwa nina ujasiri ninapowaandikia nikiwa mbali, lakini ni mwoga kusema jambo lo lote ninapokuwa pamoja nanyi. Wanadhani sababu ya kutenda yale tunayoyafanya ni kama zile za kidunia. Ninapanga kuwa jasiri sana kinyume chao watu hao hapo ninapokuja kwenu. Tafadhali ninawaomba, sitahitaji kutumia ujasiri huo kwenu. Tunaishi katika ulimwengu huu, lakini hatupigani vita yetu kama ulimwengu unavyopigana. Silaha tunazozitumia si za kibinadamu. Silaha zetu zina nguvu kutoka kwa Mungu na zinaweza kuharibu ngome za adui. Tunaharibu mabishano ya watu, na tunasambaratisha kila wazo la kiburi linalojiinua kinyume cha elimu ya Mungu. Pia tunateka kila wazo na kulitiisha ili limtii Kristo. Tuko tayari kumwadhibu kila mtu asiyetii, lakini tunataka ninyi muwe watiifu ipasavyo kwanza. Mnatakiwa kuchunguza ukweli halisi wa mambo ulio mbele ya macho yenu. Ikiwa mna uhakika kuwa ninyi ni wa Kristo, mnapaswa kukumbuka kuwa na sisi ni wa Kristo kama ninyi mlivyo wa Kristo. Inaweza kuonekana kana kwamba tunajivuna sana kupita kiasi kidogo kuhusu mamlaka ambayo Bwana ametupa sisi. Lakini alitupa mamlaka hii ili kuwatia nguvu ninyi, na sio kuwaumiza. Hivyo sitaona haya kwa lolote ambalo tumejisifu kwalo. Sitaki mfikiri kuwa najaribu kuwatisha kwa barua zangu. Wengine wanasema, “Barua za Paulo zina shuruti na matakwa mengi, Lakini anapokuwa pamoja nasi, ni mdhaifu na msemaji asiyefaa.” Watu hao wanapaswa kulielewa jambo hili: tutakapokuwa pamoja nanyi, tutatenda mambo kwa ujasiri ule ule tunaouonyesha sasa katika barua zetu. Hatujaribu kujiweka katika daraja moja na wale wanaojisifu wenyewe. Hatujilinganishi na watu hao. Wao wanatumika wenyewe kwa kujipima wenyewe, na wanajilinganisha miongoni mwao wenyewe. Hili linadhihirisha kuwa hawajui lolote. Lakini hatutajisifia lolote nje ya kazi tuliyopewa kuifanya. Tutaweka ukomo wa kujisifia kwetu katika kazi aliyotupa Mungu kuifanya, lakini kazi hii inajumuisha kazi yetu kwenu. Tungekuwa tunajivuna zaidi na zaidi ikiwa tungekuwa hatujafika kabisa kwenu. Lakini tulikuwa wa kwanza kufika kwenu na Habari Njema ya Kristo. Tumeweka ukomo wa kujivuna kwetu katika kazi ambayo ni yetu. Hatujivunii kazi ambayo wameifanya watu wengine. Tunatumaini kuwa imani yenu itaendelea kukua. Tunatumaini kuwa mtaisadia kazi yetu kukua zaidi na zaidi. Tunataka kuieneza habari njema katika maeneo ya mbali zaidi kupita mji wenu. Hatutaki kujisifia juu ya kazi ambayo imefanywa na mtu mwingine katika eneo lake. “Yeyote anayejisifu na ajisifu juu ya Bwana tu.” Kile watu wanachosema kuhusu wao wenyewe hakina maana yeyote. Cha muhimu ni ikiwa Bwana anasema kuwa wamefanya vizuri. Natamani mngekuwa na subira nami hata pale ninapokuwa mjinga kidogo. Tafadhali muwe na subira nami. Nina wivu unaotoka kwa Mungu kwa ajili yenu. Niliahidi kuwatoa ninyi kama bibi harusi kwa mume mmoja. Niliahidi kuwatoa ninyi kwa Kristo muwe bibi harusi wake aliye safi. Ila nina hofu kuwa nia zenu zitapotoshwa muache kujitoa kwa dhati na kumfuata Yesu Kristo kwa moyo safi. Hili laweza kutokea kama vile Hawa alivyodanganywa na nyoka kwa akili zake za ujanja wenye udanganyifu. Mnaonekana kuwa na subira na mtu yeyote anayekuja kwenu na kuwaeleza habari za Yesu aliye tofauti na Yesu yule ambaye sisi tuliwaambia habari zake. Mnaonekana kuwa radhi kuipokea roho au ujumbe ulio tofauti na roho na ujumbe ambao mlioupokea kutoka kwetu. Sidhani kuwa hao “mitume wakuu” ni bora kuliko mimi nilivyo. Ni kweli kuwa mimi siye mtu nilyefunzwa kwa mzungumzaji, lakini nina ufahamu wa mambo. Tumeliweka hili wazi kwenu kwa njia zote na kwa mazingira yote. Nilifanya kazi ya kutangaza Habari Njema za Mungu kwenu bila malipo. Nilijinyenyekeza ili kuwafanya ninyi kuwa wa muhimu. Je! Mwadhani nilikosea katika hilo? Nilipokea malipo toka makanisa mengine. Ilikuwa kana kwamba nimechukua fedha toka kwao ili niweze kuwatumikia ninyi. Kama nilihitaji chochote nilipokuwa nanyi, sikumsumbua yeyote kati yenu. Kina kaka waliofika kutoka Makedonia walinipa yote niliyohitaji. Sikutaka kuwa mzigo kwenu kwa namna yeyote ile. Na kamwe sitakuwa mzigo kwenu. Hakuna mtu yeyote katika jimbo lote la Akaya anayeweza kunizuia kujivuna juu ya hilo. Nasema hili katika kweli ya Kristo iliyo ndani yangu. Kwa nini siwalemei? Je! Mnadhani ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kwamba ninawapenda. Na nitaendelea kufanya kile ninachokifanya sasa, kwa sababu nataka kuwazuia watu hao wasiwe na sababu ya kujivunia. Wangependa kusema kuwa kazi ile wanayojivunia ni sawa na kazi yetu. Wao ni mitume wa uongo, watenda kazi walio wadanganyifu. Wao hujifanya kuwa ni mitume wa Kristo. Hilo halitushangazi sisi, kwa sababu hata Shetani mwenyewe hujigeuza na kujifanya kuwa malaika wa nuru. Hivyo, hiyo haitufanyi sisi kustaajabu ikiwa watumishi wa shetani watajigeuza na kujifanya kuwa watumishi wanaofanya yaliyo ya haki. Lakini mwishowe watapokea hukumu wanayostahili. Ninawaambia tena: Asiwepo yeyote wa kudhani kuwa mimi ni mjinga. Lakini kama mnadhani kuwa mimi ni mjinga, basi nipokeeni kama vile ambavyo mngempokea mjinga. Kisha nami naweza kujivuna angalau kidogo zaidi pia. Lakini mimi sizungumzi kwa namna ambavyo Bwana angelizungumza. Mimi ninajivuna kama vile mjinga. Wengi wengine wanajivuna jinsi ambavyo watu wa dunia hii wanafanya. Hivyo, nami nitajivuna kwa namna hiyo. Mna busara, hivyo mtamvumilia kwa furaha mjinga! Nasema haya kwa sababu mnamvumilia hata mtu yule anayewatumia vibaya. Mnawavumilia wale wanaowarubuni akili na kudhani kuwa wao ni bora kuliko ninyi, au wanaowapiga usoni! Ninaona aibu kusema haya, lakini tulikuwa “dhaifu sana” kuyafanya mambo kama hayo kwenu. Lakini kama kuna mtu aliye jasiri vya kutosha kujivuna, nami nitajivuna pia. (Ninaongea hivi kama mjinga.) Je, watu hao ni Wayahudi? Mimi pia. Je, ni Waebrania? Mimi pia. Je, wanatoka katika familia ya Ibrahimu? Mimi pia. Je, wanamtumikia Kristo? Mimi ninamtumikia zaidi sana. (Je, mimi ni mwendawazimu kuongea kwa jinsi hii?) Nimefanya kazi kwa juhudi kuliko wao. Nimekuwa gerezani mara nyingi. Nimepigwa vibaya sana. Nimekuwa katika hali za hatari ya kufa mara nyingi. Mara tano Wayahudi wamenipa adhabu ya viboko 39. Mara tatu katika nyakati tofauti nimepigwa kwa fimbo. Mara moja nilikuwa karibu kuuawa kwa kupigwa kwa mawe. Mara tatu nimevunjikiwa na merikebu, na mara moja katika hizo nilikesha usiku na kushinda kutwa nzima tukielea baharini. Katika safari zangu za mara kwa mara nimekuwa katika hatari za kwenye mito, majambazi, watu wangu wenyewe, na toka kwa watu wasio Wayahudi. Nimekuwa katika hatari mijini, katika maeneo wasioishi watu, na katika bahari. Na nimekuwa katika hatari za watu wanaojifanya kuwa waamini lakini siyo waamini. Nimefanya kazi ngumu na za kuchosha, na mara nyingi sikuweza kulala usingizi. Nimekuwa mwenye njaa na kiu. Mara nyingi nimekosa kula chakula. Nimekuwa katika hali ya baridi na kutokuwa na nguo za kujifunika. Na kuna matatizo mengine mengi zaidi. Mojawapo ya hayo ni mzigo nilio nao kila siku wa majukumu yangu: Ninawaza juu ya makanisa yote. Ninajisikia kuwa mdhaifu kila mara mtu mwingine anapokuwa dhaifu. Ninapata hasira sana pale mtu yeyote anapoingizwa dhambini. Ikiwa ni lazima nisifu, nitajisifu katika vitu vinavyonidhihirisha kuwa mimi ni dhaifu. Mungu ajua kuwa sisemi uongo. Yeye ni Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, na anapaswa kutukuzwa milele. Nilipo kuwa Dameski, gavana wa mfalme Areta alitaka kunikamata, hivyo aliweka walinzi nje ya malango ya jiji. Lakini baadhi ya marafiki wakaniweka ndani ya kikapu. Kisha wakaniteremsha chini kupitia dirisha lililokuwa kwenye katika ukuta wa mji. Hivyo nikamtoroka gavana. Inanipasa kuendelea kujivuna juu yangu mwenyewe. Hiyo haitasaidia, lakini nitazungumza juu ya maono na mafunuo kutoka kwa Bwana. Ninamjua mtu mmoja katika Kristo aliyechukuliwa juu katika mbingu ya tatu. Hili lilitokea miaka 14 iliyopita. Sifahamu ikiwa mtu huyu alikuwa ndani ya mwili wake au nje ya mwili wake, lakini Mungu anajua. Na ninajua kuwa mtu huyu alichukuliwa juu paradiso. Sijui kama alikuwa katika mwili wake au nje ya mwili wake. Mungu pekee ndiye anajua. Lakini mtu huyu aliyasikia mambo ambayo hana uwezo wa kuyasimulia. Alisikia mambo ambayo mtu yeyote anaruhusiwa kuyasema. *** Nitajivunia mtu wa namna hiyo, lakini sitajivuna juu yangu mwenyewe. Nitajivuna tu katika madhaifu yangu. Lakini ikiwa nilitaka kujivuna, sitakuwa nikizungumza kama mjinga, kwa sababu ningekuwa nasema iliyo kweli. Lakini sitajivuna tena zaidi, kwa sababu sitaki watu wanifikirie kwa ubora zaidi kuliko wanavyoniona nikitenda ama kusikia ninayosema. Lakini imenipasa kutojivuna zaidi juu ya mambo ya ajabu yaliyoonyeshwa kwangu. Kwa sababu hiyo nilipewa tatizo lenye maumivu; malaika toka kwa Shetani; aliyetumwa kwangu kunitesa, ili nisiweze kufikiri kwamba mimi ni bora zaidi kuliko watu wengine. Nilimwomba Bwana mara tatu kuliondoa tatizo hili kwangu. Lakini Bwana alisema, “Neema yangu ndiyo unayoihitaji. Ni pale tu unapokuwa dhaifu ndipo kila kitu kinapoweza kufanyika katika uwezo wangu.” Hivyo nitajivunia udhaifu wangu kwa furaha. Hapo ndipo uweza wa Kristo unaweza kukaa ndani yangu. Ndiyo, nina furaha kuwa na madhaifu ikiwa ni kwa ajili ya Kristo. Nina furaha kuaibishwa na kupitia magumu. Nina furaha ninapoteswa na kupata matatizo, kwa sababu ni pale nilipodhaifu ndipo ninapokuwa na nguvu. Nimekuwa nikizungumza kama mjinga, lakini ninyi ndiyo mliosababisha nikafanya hivyo. Ninyi ndiyo mnaopaswa kuzungumza mema juu yangu. Mimi si kitu, lakini mimi si myonge kwa njia yeyote ile kwa hao “mitume wakuu”. Nilipokuwa pamoja nanyi, nilifanya kwa uvumilivu wote vitu vilivyo nilidhihirisha kuwa mimi ni mtume kwa ishara, maajabu na miujiza. Kwa hiyo mlipokea kila kitu ambacho makanisa yote yalipata. Kitu kimoja tu ndicho kilikuwa cha tofauti na cha kipekee: Sikuwa mzigo au msumbufu kwenu. Mnisamehe kwa hilo. Niko tayari sasa kuwatembelea kwa mara ya tatu, na sitakuwa mzigo kwenu. Mimi sitafuti kitu chochote kilicho chenu. Ninawataka ninyi tu. Watoto wasiweke akiba vitu vya kuwapa wazazi wao. Wazazi wanapaswa kuweka akiba vitu vya kuwapa watoto wao. Kwa hiyo ninayo furaha kutumia kile nilichonacho kwa ajili yenu. Na mimi mwenyewe nitajitoa kikamilifu kwa ajili yenu. Je, kama upendo wangu kwenu utakuwa mkubwa, upendo wenu kwangu utapungua? Ni wazi kuwa sikuwa mzigo kwenu, lakini baadhi yenu wanadhani kuwa nilikuwa mjanja, na kutumia hila kuwaweka mtegoni. Je, niliwadanganya kwa kuwatumia mtu yeyote kati ya wale niliyowatuma kwenu? Mnafahamu kuwa sikufanya hivyo. Nilimwomba Tito aje kwenu, na nilimtuma kaka yetu afuatane naye. Tito hakuwadanganya, je alifanya hivyo? Hapana! Na kwa hiyo mjue kuwa matendo yangu na tabia yangu ilikuwa ya dhati kama ilivyokuwa kwake. Je! Mnadhani tumekuwa tukijitetea? Hapana, tunasema haya katika Kristo na mbele za Mungu. Ninyi ni rafiki zetu wapendwa, na kila tunachofanya tunakifanya ili muwe imara. Ninafanya hivi kwa sababu ninaogopa kuwa nitakapokuja, hamtakuwa kama vile ninavyotaka muwe. Na pia nina wasiwasi kuwa sitakuwa kwa namna ile mnayotaka mimi niwe. Nina hofu kuwa nitawakuta mkibishana, wenye wivu, wenye hasira, mkipigana kwa ubinafsi wenu, wenye misemo mibaya, watetaji, wenye kiburi, na machafuko huko. Nina wasiwasi kuwa nitakapokuja kwenu, Mungu wangu ataninyenyekeza tena mbele yenu. Nitalazimika kuomboleza kwa ajili ya wale ambao wametenda dhambi. Wengi wao hawajarejea na kutubia maisha yao ya uovu, dhambi za zinaa, na mambo ya aibu waliyotenda. Hii itakuwa ni safari yangu ya tatu kuwatembelea. Na mkumbuke, “Kila shitaka ni lazima lithibitishwe na mashahidi wawili au watatu wanaosema kuwa jambo hilo ni la kweli.” Nilipokuwa pamoja nanyi mara ya pili, nilitoa maonyo kwa wale waliotenda dhambi. Sipo hapo sasa, ila natoa onyo lingine kwao na kwa yeyote aliyetenda dhambi: Nitakapo kuja tena kwenu, nitawaadhibu walio miongoni mwenu ambao bado wanatenda dhambi. Mnatafuta uthibitisho kuwa Kristo anasema kupitia mimi. Uthibitisho wangu ni kuwa yeye si dhaifu kuwashughulikia bali yeye anaonesha uweza wake miongoni mwenu. Ni kweli kuwa Kristo alikuwa dhaifu alipouawa msalabani, lakini yu hai kwa nguvu za Mungu. Ni kweli pia kwamba twashiriki unyonge wake, lakini kwa kushughulika nanyi, tutakuwa hai pamoja nae katika uweza wa Mungu. Jiangalieni ninyi wenyewe. Mjipime ninyi wenyewe mkaone kama mngali mnaishi katika imani. Hamtambui kuwa Kristo Yesu yu ndani yenu? La mkishindwa jaribio hilo; ikiwa hamtakuwa mkiishi katika imani; basi Kristo hayumo ndani yenu. Lakini ni matumaini yangu kuwa mtagundua ya kwamba hatujashindwa jaribio hilo. Tunawaombea kwa Mungu msifanye lolote lililo baya. Tunachojali hapa si kwamba watu waone kuwa tumeshinda jaribio katika ile kazi tuliyofanya pamoja nanyi. Tunachokitaka zaidi ni ninyi kufanya lililo jema, hata ikiwa itaonekana kuwa tumeshindwa jaribio. Hatuwezi kufanya lolote lililo kinyume na kweli bali lile linalodumisha kweli. Tunafuraha kuonekana tu wadhaifu ikiwa ninyi mko imara. Na hili ndilo tunaloomba, kwamba maisha yenu yatakamilishwa katika haki tena. Ninaandika haya kabla sijaja kwa kuwa niko mbali nanyi ili nijapo nisilazimike kutumia mamlaka kuwaadhibu. Bwana alinipa mamlaka hayo kuwaimarisha, na sio kuwaharibu. Sasa, wapendwa dada zangu na kaka zangu mjazwe furaha. Jitahidini kutengeneza njia zenu, fanyeni nilichowaomba kufanya. Mpatane kila mmoja na mwenziwe, na ishini katika amani. Ndipo Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Msalimiane kwa salamu maalum ya watu wa Mungu. Watakatifu wote wa Mungu hapa nao wanawasalimu. Ninawaombea ili ninyi nyote mfurahie neema ya Bwana Yesu Kristo, upendo wa Mungu, na Ushirika wa Roho Mtakatifu. Salamu kutoka kwa mtume Paulo. Sikutumwa na kundi lolote la watu au mtu yeyote hapa duniani niwe mtume. Sikupewa mamlaka yangu na mwanadamu yeyote. Nilipewa mamlaka haya moja kwa moja kutoka kwa Kristo Yesu na Mungu Baba, aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu. Salamu pia kutoka kwa wote walio familia ya Mungu, walio pamoja nami. Kwa makanisa yaliyoko Galatia: Namwomba Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo awe mwema kwenu na awape neema na amani. Yesu alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu ili atuweke huru kutoka katika uovu wa ulimwengu huu tunamoishi. Hili ndilo Mungu Baba yetu alitaka. Mungu Baba yetu anastahili utukufu milele na milele! Amina. Wakati mfupi tu uliopita Mungu aliwaita mkamfuata. Aliwaita katika neema yake kwa njia ya Kristo. Lakini sasa nashangazwa kwamba kwa haraka hivi mmegeuka mbali na kuamini kitu kingine tofauti kabisa na Habari Njema tuliyowahubiri. Hakuna ujumbe mwingine wa Habari Njema, lakini baadhi ya watu wanawasumbua. Wanataka kuibadili Habari Njema ya Kristo. Tuliwahubiri ninyi ujumbe wa Habari Njema tu. Hivyo laana ya Mungu impate mtu yeyote yule anayewahubiri ninyi ujumbe ulio tofauti, hata ikiwa ni mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni! Nitalisema tena lile nililolisema hapo mwanzo. Ninyi mmekwishaipokea Habari Njema. Yeyote atakayewahubiri kitu kingine tofauti na ile Habari Njema mliyoipokea, basi mjue kwamba Mungu atamlaani mtu huyo! Sasa mnafikiri ninajaribu kuwapendeza wanadamu? Hapana, ninataka kumpendeza Mungu siyo wanadamu. Kama ningekuwa najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumwa wa Kristo. Ndugu zangu, ninawataka mjue kuwa ujumbe wa Habari Njema niliowaambia haukuandaliwa na mtu yeyote. Sikuupata ujumbe wangu kutoka kwa mwanadamu yeyote. Habari Njema siyo kitu nilichojifunza kutoka kwa watu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia Habari Njema ninayowahubiri watu. Mmesikia juu ya mwenendo wangu hapo zamani nilipokuwa mfuasi hodari wa dini ya Kiyahudi. Nililitesa kwa nguvu kanisa la Mungu, nikiwa na shabaha ya kuliangamiza kabisa. Nilipata maendeleo makubwa katika dini ya Kiyahudi kwa kufanya kazi na kusoma kwa bidii kwa sababu nilikuwa mwaminifu kwa desturi za baba zetu. Lakini Mungu alikuwa na mpango maalumu kwa ajili yangu hata kabla sijazaliwa. Hivyo aliniita kwa neema yake. Na ilimpendeza kumfunua Mwanaye ili niweze kuwahubiri Habari Njema watu wasio Wayahudi. Hicho ndicho nilichofanya baada ya hapo. Sikuomba ushauri ama msaada wowote kutoka kwa mtu yeyote. Sikwenda Yerusalemu kuwaona wale waliokuwa mitume kabla mimi sijawa mtume. Badala yake, kwanza nilienda moja kwa moja Arabia. Kisha baadaye, nikarudi katika mji wa Dameski. Miaka mitatu baadaye nilikwenda Yerusalemu kumwona Petro. Nilikaa naye kwa siku 15. Sikuonana na mtume mwingine yeyote, isipokuwa Yakobo mdogo wake Bwana peke yake. Mungu anajua kuwa hakuna ninachowaandikia kisicho cha kweli. Baadaye, nilielekea katika majimbo ya Shamu na Kilikia. Lakini kwa wakati ule, makanisa ya Kristo yaliyokuwa Uyahudi yalikuwa bado hayajanifahamu mimi binafsi. Walikuwa wamesikia tu juu yangu: “Mtu huyu alikuwa anatutesa. Lakini sasa anawaambia watu juu ya imani ile ile aliyojaribu kuiangamiza huko nyuma.” Waamini hawa walimsifu Mungu kwa sababu yangu. Baada ya miaka 14 nilirudi tena Yerusalemu nikiwa na Barnaba na nilimchukua Tito pia. Nilikwenda kule maana Mungu alinionyesha kuwa ninapaswa kwenda. Niliwafafanulia Habari Njema kama nilivyoihubiri kwa watu wasio Wayahudi. Pia nilikutana faragha na wale waliokuwa wanatazamiwa kuwa viongozi. Nilitaka niwe na uhakika kuwa tulikuwa tunapatana ili kazi yangu ya nyuma na ile niliyokuwa naifanya sasa zisipotee bure. Tito, aliyekuwa pamoja nami ni Myunani. Hata hivyo viongozi hawa hawakulazimisha kumtahiri. Tulihitaji kuyazungumzia matatizo haya, kwa sababu wale waliojifanya kuwa ni ndugu zetu walikuja kwenye kundi letu kwa siri. Waliingia kama wapelelezi kutafiti kuhusu uhuru tuliokuwa nao ndani ya Kristo Yesu. Walitaka watufanye sisi watumwa, lakini hatukujiweka chini ya chochote ambacho hawa ndugu wa uongo walikitaka. Tulitaka ukweli wa Habari Njema ubaki ule ule na hatimaye uwafikie na ninyi. Na watu wale ambao walihesabiwa kuwa viongozi muhimu hawakuongeza lolote katika ujumbe wa Habari Njema niliyowahubiria watu. (Haijalishi kwangu kuwa walikuwa wa “muhimu” au la. Kwa Mungu binadamu wote ni sawa.) Lakini viongozi hawa waliona kuwa Mungu alinipa kazi maalumu ya kuhubiri Habari Njema kwa wasio Wayahudi, kama vile alivyomwagiza Petro kufanya kazi hiyo hiyo ya kuhubiri Habari Njema miongoni mwa Wayahudi. Mungu alimpa Petro uwezo wa kufanya kazi kama mtume lakini kwa walio Wayahudi. Mungu akanipa mimi pia uwezo wa kufanya kazi kama mtume, lakini kwa wasiokuwa Wayahudi. Yakobo, Petro na Yohana walikuwa viongozi muhimu kanisani. Hawa wakaona kuwa Mungu alinipa kipaji hiki maalumu cha huduma, hivyo wakatupa mkono wa shirika mimi pamoja na Barnaba. Wakakubali kuwa sisi tutaendelea kufanya kazi miongoni mwao wasio Wayahudi, na wao wataendelea kufanya kazi miongoni mwao walio Wayahudi. Wakatuomba jambo moja tu, ya kwamba tukumbuke kuwahudumia waaminio walio maskini. Na kwa hakika hili lilikuwa jambo nililojitahidi kufanya. Petro alipokuja Antiokia, alifanya kitu ambacho hakikuwa sahihi. Nami nikampinga, kwa sababu hakika alikuwa na hatia mbele za Mungu. Hivi ndivyo ilivyotokea: Petro alipokuja Antiokia, hapo awali kabla ya Wayahudi kufika, alikula na kujumuika na wasio Wayahudi. Lakini baada ya Wayahudi kufika kutoka kwa Yakobo, Petro akajitenga na wasio Wayahudi. Akaacha kula pamoja nao kwa sababu aliwaogopa Wayahudi. Hivyo Petro akafanya kama mnafiki, na waamini wengine pale Antiokia wakaungana naye katika unafiki huo. Wakamfanya hata Barnaba naye kuwa mnafiki kama wao. Hawakuwa wakiifuata kweli ya Habari Njema. Nilipoona hili, nilimweleza Petro mbele ya kila mtu. Nilisema, “Petro, wewe ni Myahudi, lakini huenendi kama Myahudi. Unaenenda kama mtu asiye Myahudi. Hivyo kwa nini unajaribu kuwalazimisha wale wasio Wayahudi kuenenda kama Wayahudi? Sisi ni Wayahudi kwa kuzaliwa. Hatukuzaliwa tukiwa ‘watenda dhambi’, kama vile Wayahudi wanavyowaita wale wasio Wayahudi. Lakini tunajua kuwa hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Ni kwa kuamini katika Yesu Kristo ndiko kunamfanya mtu ahesabiwe haki mbele za Mungu. Hivyo hata nasi Wayahudi tumeiweka imani yetu katika Kristo Yesu, kwa sababu tulitaka kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Na tumehesabiwa haki kwa imani ya Yesu Kristo, siyo kwa sababu tuliifuata sheria. Naweza kusema hili kwa sababu hakuna anayeweza kuhesabiwa haki kwa kuifuata Sheria ya Musa. Kwa hiyo tunaamini uhusiano wetu kwa Kristo utatufanya tuhesabiwe haki mbele za Mungu. Ikiwa hiyo inatufanya tuonekane kama ‘watenda dhambi’ wasio Wayahudi, je itakuwa na maana kuwa Kristo anasababisha dhambi kuongezeka. Kwa hakika sivyo? Sheria ilijenga ukuta baina yetu Wayahudi na watu wengine wote, ukuta ambao nilijitahidi kuuvunja. Kweli nitakosea sana kuujenga tena ukuta huo. Sheria yenyewe iliyafikisha mwisho maisha yangu chini ya sheria. Nikafa katika sheria hiyo na kuwa huru ili niweze kuishi kwa ajili ya Mungu. Nimepigiliwa misumari msalabani pamoja na Kristo. Hivyo siyo mimi ninayeishi sasa; ni Kristo ndiye anayeishi ndani yangu. Bado naishi katika mwili wangu, lakini naishi kwa imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda na kujitoa mwenyewe kuniokoa mimi. Si mimi ninayeikataa neema ya Mungu kama vile haina manufaa yoyote. Kwa sababu ikiwa kwa kuifuata sheria ndivyo watu wanahesabiwa haki mbele za Mungu, basi Kristo alikufa pasipo faida!” Ninyi watu wa Galatia, je mmepoteza fahamu zenu? Nilidhani mmeelewa kwa nini Yesu Kristo alisulubiwa msalabani! Niliwaeleza wazi kabisa jambo hilo, kama vile kuchora na kupaka rangi picha mbele ya macho yenu. Je, kuna mtu yeyote aliyewaloga mkasahau? Niambieni jambo hili moja: Ni jinsi gani mlimpokea Roho? Je, mlimpokea Roho kwa kufuata sheria? Hapana, mlimpokea Roho kwa sababu ya ujumbe kuhusu Yesu unaoleta imani. Mliyaanza maisha yenu mapya pamoja na Roho. Inakuwaje sasa mdhani kuwa mnaweza kukamilishwa na kitu kinyonge kama tohara kilichofanyika katika miili yenu? Basi mmepoteza fahamu zenu! Je, mlipata uzoefu huo mwingi pasipo manufaa yoyote? Sidhani kama hivyo ndivyo! Je, Mungu anawapa ninyi Roho na kutenda miujiza miongoni mwenu kwa kuwa mnaifuata sheria? Hapana sivyo! Mungu anawapa ninyi baraka hizi kwa njia ya ujumbe unaoleta imani katika kumwamini Yesu. Maandiko yanasema kitu hicho hicho kuhusu Ibrahimu. “Ibrahimu alimwamini Mungu, na Mungu akaikubali imani yake na akamhesabia haki.” Hivyo mnapaswa kuelewa kuwa watoto sahihi wa Ibrahimu ni wale walio na imani. Maandiko yalieleza ambacho kingetokea katika siku zijazo. Maandiko haya yalisema kwamba Mungu angewafanya wasio Wayahudi kuwa wenye haki kwa njia ya imani. Mungu alizisema Habari Njema hizi kwa Ibrahimu kabla haijatokea. Mungu alimwambia Ibrahimu, “Kwa kukubariki wewe, nitawabariki watu wote duniani.” Kwa hiyo, wale wote wanaoweka imani yao kwa Mungu ndiyo wanaobarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwaminifu. Lakini watu wale wanaodhani kuwa kutii sheria ndicho kitu muhimu sana daima hukaa chini ya tishio la laana. Kama vile Maandiko yanavyosema, “Amelaaniwa mtu yeyote atakayeacha kuzishika na kuzitii sheria hizi zote.” Hivyo ni dhahiri kuwa hakuna anayeweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Maandiko yanasema, “Mwenye haki mbele za Mungu ataishi kwa imani.” Sheria haitegemei imani. Hapana, inasema kuwa njia pekee ambayo mtu anaweza kupata uzima kwa njia ya sheria ni kwa kutii amri zake. Sheria inasema kuwa sisi Wayahudi tuko chini ya laana kwa kutokuitii daima. Lakini Kristo alituweka huru kutoka katika laana hiyo. Alikubali kulaaniwa na sheria ili atuokoe. Maandiko yanasema, “Yeyote anayening'inizwa mtini yuko chini ya laana.” Kwa sababu ya yale aliyoyafanya Kristo Yesu, baraka ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu zilitolewa pia kwa wasio Wayahudi. Kristo alikufa ili kwamba kwa kumwamini sisi sote, Wayahudi na wasio Wayahudi, tuweze kumpokea Roho ambaye Mungu aliahidi. Ndugu zangu, hebu niwape mfano kutoka maisha ya kila siku: Fikiri kuhusu makubaliano ambayo mtu hukubaliana na mwingine. Baada ya makubaliano hayo kufanywa rasmi, hakuna anayeweza kuongeza chochote kwenye makubaliano hayo na hakuna anayeweza kulipuuza. Mungu aliweka agano kwa Ibrahimu na uzao wake. Maandiko hayasemi, “na kwa ajili ya uzao wenu”. Hilo lingekuwa na maana ya watu wengi. Lakini linasema, “na kwa uzao wako”. Hiyo ina maana ya uzao mmoja tu, na uzao huo ni Kristo. Hii ndiyo maana yangu: Agano ambalo Mungu aliliweka na Ibrahimu lilifanywa rasmi na Mungu muda mrefu kabla ya kuja kwa sheria. Sheria ilikuja miaka 430 baadaye. Hivyo sheria haingeweza kulifuta agano hilo na kuibadili ahadi ya Mungu. Baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake hazipatikani kwa njia ya sheria. Ikiwa ingekuwa hivyo, basi isingekuwa ahadi ya Mungu inayotuletea sisi baraka hiyo. Lakini Mungu aliitoa bure baraka yake kwa Ibrahamu kama agano. Hivyo kwa nini sheria ilitolewa? Sheria ililetwa baadaye kwa sababu ya makosa wanayotenda watu. Lakini sheria ingeendelea kutumika hadi kuja kwa Uzao wa Ibrahimu. Huyu ni Uzao unaotajwa katika agano lililotolewa na Mungu. Lakini sheria ilitolewa kupitia malaika na malaika walimtumia Musa kama mpatanishi wa kuwapa watu sheria. Hivyo mpatanishi anahitajika pale ambapo upande mmoja unapaswa kufikia mapatano. Lakini Mungu ambaye ni mmoja, hakumtumia mpatanishi alipompa ahadi Ibrahimu. Je, hili lamaanisha kwamba sheria hutenda kazi kinyume na ahadi za Mungu? La hasha. Sheria iliyotolewa kamwe haikuwa na uwezo wa kuwaletea watu maisha mapya. Ingekuwa hivyo, basi tungehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Lakini hilo halikuwa kusudi la sheria. Maandiko yanauweka ulimwengu wote chini ya udhibiti wa dhambi kama aina ya kifungo gerezani. Ili kile ambacho Mungu aliahidi kipokelewe kwa njia ya imani katika Yesu Kristo. Hii hutolewa kwa wale wanaomwamini. Kabla ya aliye mwaminifu kuja, sheria ilituweka sisi kama wafungwa. Hatukuwa huru hadi imani hii inayokuja ilipofunuliwa kwetu. Nina maana kuwa sheria ilikuwa ni mlezi aliyetusimamia tu hadi Kristo alipokuja. Baada ya kuja kwake, tungefanyika kuwa wenye haki mbele za Mungu kwa njia ya imani. Sasa kwa sababu imani hii imekuja, hatuhitaji tena kusimamiwa na kulelewa na sheria. Hii ni kwa sababu ninyi nyote ni mali ya Kristo Yesu na ni watoto wa Mungu kwa njia ya imani. Ndiyo, nyote mlibatizwa ili muunganike na Kristo. Hivyo sasa Kristo anawafunika kabisa kama kubadilisha nguo mpya kabisa. Sasa, ndani ya Kristo haijalishi kama wewe u Myahudi au Myunani, mtumwa au huru, mwanaume au mwanamke. Wote mko sawa katika Kristo Yesu. Na kwa vile ninyi ni wa Kristo, hivyo ninyi wazaliwa wa Ibrahamu. Ninyi ndiyo mtakaopokea baraka zote ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu. Ninalolisema ni hili: Wakati mrithi wa vyote alivyomiliki baba yake bado ni mdogo, hana tofauti yo yote na mtumwa. Haijalishi kuwa anamiliki vitu vyote. Wakati wa utoto bado anapaswa kuwatii wale waliochaguliwa kumtunza. Lakini anapoufikia umri ambao baba yake ameuweka, anakuwa huru. Ndivyo ilivyo hata kwetu sisi. Mwanzoni tulikuwa kama watoto, tukiwa watumwa wa mamlaka za uovu zinazoutawala ulimwengu huu wa sasa. Lakini wakati sahihi ulipofika, Mungu akamtuma Mwanaye, aliyezaliwa na mwanamke na akaishi chini ya sheria. Mungu alifanya hivi ili aweze kuwaweka huru wale waliokuwa chini ya sheria. Kusudi la Mungu lilikuwa kutuasili sisi kama watoto wake. Ninyi sasa ni watoto wa Mungu. Na ndiyo sababu Mungu amemtuma Roho wa Mwanaye mioyoni mwetu. Huyo Roho aliye ndani yetu hulia “Aba, yaani Baba.” Sasa ninyi si watumwa kama mwanzo. Ni watoto wa Mungu, na mtapokea kila kitu ambacho Mungu aliwaahidi watoto wake. Hii yote ni kwa sababu ya yale ambayo Mungu amewatendea ninyi. Zamani hamkumjua Mungu. Mlikuwa watumwa wa miungu isiyokuwa halisi. Lakini sasa mnamjua Mungu wa kweli. Hakika, Mungu ndiye anayewajua ninyi. Hivyo kwa nini sasa mnavigeukia vikosi dhaifu na visivyo na manufuaa yoyote mlivyovifuata hapo mwanzo? Mnataka kuwa watumwa wa mambo haya tena? Inanipa wasiwasi kwa kuwa mnaadhimisha siku, miezi, misimu na miaka. Nina hofu ya kuwa nimefanya kwa bidii kazi bure kwa ajili yenu. *** Ndugu zangu, naomba mniige mimi kama ambavyo mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunikosea kwa jambo lololote. Mnajua kuwa nilikuja kwenu mara ya kwanza kwa sababu nilikuwa mgonjwa. Ndipo nilipowaeleza ninyi Habari Njema. Ugonjwa wangu uliwaelemea. Hata hivyo hamkunikataa kutokana na fadhaa ama hofu. Bali, mlinikaribisha kama vile nilikuwa malaika kutoka kwa Bwana. Mlinipokea kama vile nilikuwa Kristo Yesu mwenyewe! Mlikuwa na furaha sana wakati huo. Nini kimetokea kwa imani yenu ya awali kwamba mimi nilikuwa mtu niliyebarikiwa kipekee na Mungu? Naweza kusema bila shaka yoyote kwamba mngeliweza kufanya kitu chochote kunisaidia. Kama ingeliwezekana, mngeliyang'oa hata macho yenu na kunipa mimi. Je, nimekuwa sasa adui yenu kwa sababu nawaambia ukweli? Watu hawa wanajitahidi sana kuonesha kuvutiwa nanyi, lakini hiyo siyo nzuri kwenu. Wanataka kuwashawishi ninyi ili mtugeuke sisi na kuambatana nao. Inapendeza daima kuwa na mtu anayevutiwa nawe katika jambo lililo jema. Hivyo ndivyo nilivyofanya nilipokuwa pamoja nanyi. Siku zote inapendeza, na si pale tu mimi nikiwapo. Watoto wangu wadogo, nasikia uchungu tena kwa ajili yenu, kama mama anayejifungua. Nitaendelea kusikia uchungu huu mpaka watu watakapofikia kumwona Kristo wawatazamapo ninyi. Natamani ningekuwa nanyi sasa. Ndipo labda ninapoweza kubadilisha namna ninavyoongea nanyi. Sasa sielewi nifanye nini juu yenu. Baadhi yenu mnataka kuwa chini ya sheria. Niambieni, mnajua sheria inavyosema? Maandiko yanasema kwamba Ibrahimu alikuwa na wana wawili. Mama wa mwana mmoja alikuwa ni mjakazi, na mama wa mwana mwingine alikuwa wa mwanamke aliye huru. Mwana wa Ibrahimu kutoka kwa mjakazi alizaliwa kwa namna ya kawaida ya kibinadamu. Lakini mwana kutoka kwa mwanamke aliyekuwa huru alizaliwa kwa sababu ya ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu. Habari hii ina maana nyingine kwenu. Wanawake wawili ni sawa na maagano mawili baina ya Mungu na watu wake. Agano moja ni sheria ambayo Mungu aliifanya katika Mlima Sinai, inayowafanya watu wawe watumwa. Mwanamke aliyeitwa Hajiri yuko kama agano la kwanza. Hivyo Hajiri anauwakilisha Mlima Sinai uliopo Arabia. Na anafanana na Yerusalemu wa sasa, kwa sababu mji huu uko utumwani pamoja na watu wake. Lakini Yerusalemu ya mbinguni ulio juu uko kama mwanamke aliye huru, ambaye ndiye mama yetu. Maandiko yanasema, “Ufurahi mwanamke, wewe uliye tasa. Ufurahi kwani hukuwahi kuzaa. Piga kelele na ulie kwa furaha! Hukupata uchungu wa kuzaa. Mwanamke aliye peke yake atapata watoto zaidi zaidi ya mwanamke aliye na mume.” Ndugu zangu, ninyi ni watoto mliozaliwa kwa sababu ya ahadi ya Mungu, kama Isaka alivyozaliwa. Lakini mwana mwingine wa Ibrahimu, aliyezaliwa kwa njia ya kawaida, alisababisha matatizo kwa yule aliyezaliwa kwa nguvu ya Roho. Ndivyo ilivyo leo. Lakini Maandiko yanasemaje? “Mfukuze mjakazi na mwanawe! Mwana wa mwanamke aliye huru atapokea kila kitu alicho nacho baba yake, lakini mwana wa mjakazi hatapokea kitu.” Hivyo, kaka na dada zangu, sisi si watoto wa mjakazi. Ni watoto wa mwanamke aliye huru. Sasa tuko huru, kwa sababu Kristo alituweka huru ili tuweze kuishi tukiufurahia uhuru huo. Hivyo muwe imara katika uhuru huo. Msimruhusu mtu yeyote awaingize utumwani tena. Sikilizeni! Mimi Paulo nawaambia kwamba ikiwa mtakubali kutahiriwa, basi Kristo hatakuwa na manufaa kwenu. Tena, ninamwonya kila mtu atakayeruhusu atahiriwe, kwamba akifanya hivyo itampasa aifuate sheria yote. Ikiwa utajaribu kufanyika mwenye haki mbele za Mungu kwa njia ya sheria, maisha yako na Kristo yamepotea, kwani umeiacha neema ya Mungu. Ninasema hivi kwa sababu tumaini letu la kufanywa wenye haki mbele za Mungu huja kwa imani. Na kwa nguvu ya Roho kwa njia ya imani, tunangoja kwa utulivu na kwa matumaini yenye ujasiri hukumu ya Mungu inayotuweka huru. Mtu anapokuwa wa Kristo Yesu, vyote kutahiriwa ama kutotahiriwa havina nguvu ya kuleta manufaa yoyote. Lakini kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu imani inatenda kazi kupitia upendo. Mlikuwa mnapiga mbio vizuri sana. Ni nani aliyewafanya mkaacha kuitii kweli? Hakika hakuwa yule aliyewachagua. Mjihadhari! “Chachu ndogo tu hufanya mkate wote mzima uumuke.” Nimeridhika moyoni mbele za Bwana kuwa hamtafikiri vinginevyo. Mtu yule anayewasumbua atahukumiwa hata angekuwa nani? Kaka na dada zangu, sifundishi kuwa ni lazima mwanaume atahiriwe. Kama nitaendelea kuwafundisha wanaume watahiriwe, kwa nini watu bado wanaendelea kunitesa? Ikiwa bado nafundisha tohara, basi ujumbe wangu kuhusu msalaba hautaendelea kuwa tatizo. Natamani watu hao wanaowasumbua wangeongeza na kuhasi juu ya tohara yao. Ndugu na dada zangu, Mungu aliwaita ili muwe huru. Lakini msiutumie uhuru wenu kama udhuru wa kutimiza yale yote mnayoyapenda, badala yake, msaidiane ninyi kwa ninyi kwa upendo. Sheria yote imepewa muhtasari katika amri hii moja tu, “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Ikiwa mtaendelea kuumizana na kuraruana, muwe waangalifu, vinginevyo mtaangamizana ninyi kwa ninyi. Hivyo ninawaambieni, ishini kama Roho anavyowaongoza. Hapo hamtatenda dhambi kutokana na tamaa zenu mbaya. Utu wenu wa dhambi unapenda yale yaliyo kinyume cha Roho, na Roho anataka yale yaliyo kinyume na utu wa dhambi. Hao siku zote hushindana wao kwa wao. Kwa jinsi hiyo ninyi hamko huru kufanya chochote mnachotaka kufanya. Lakini mkimruhusu Roho awaongoze, hamtakuwa chini ya sheria. Mambo mabaya yanayofanywa na mwili wa dhambi ni dhahiri: uasherati, tabia chafu, kufanya mambo yenye kuleta aibu, kuabudu miungu wa uongo, kushiriki mambo ya uchawi, kuwachukia watu, kuanzisha mafarakano, kuwa na wivu, hasira ama choyo, kusababisha mabishano na kujigawa kimakundi na kuwatenga wengine, kujawa na husuda, kulewa pombe, kushiriki karamu zenye ulafi na uasi mwingi na kufanya mambo yanayofanana na hayo. Ninawatahadharisha mapema kama nilivyowatahadharisha mwanzo: Watu wanaofanya mambo hayo hawatahesabiwa kama watoto watakaourithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda linalozaliwa na Roho katika maisha ya mtu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole, na kiasi. Hakuna sheria juu ya mambo kama haya. Wale walio wa Kristo Yesu wameusulubisha udhaifu wao wa kibinadamu pamoja na tamaa zake za dhambi na zile za mwili. Wameachana na utu wao wa kale wenye hisia za ubinafsi na uliotaka kufanya mambo maovu. Tunayapata maisha yetu mapya kutoka kwa Roho, hivyo tunapaswa kuufuata uongozi wa Roho. Tusijivune na kujisifu juu yetu wenyewe. Hatupaswi kuchokozana kwa mashindano baina yetu ama kuoneana wivu. Ndugu zangu, ikiwa mmoja wenu atakosea, ninyi mnaomfuata Roho mnapaswa kumwendea yule anayetenda dhambi. Msaidieni mtu huyo awe mwenye haki tena. Mfanye hivyo kwa njia ya upole, na muwe waangalifu, kwa maana nanyi pia mnaweza kujaribiwa kutenda dhambi. Msaidiane ninyi kwa ninyi katika kubeba mizigo yenu. Mnapofanya hivi, mtakuwa mnatimiza yote ambayo sheria ya Kristo imewaagiza kufanya. Maana mtu akijiona kuwa yeye ni wa muhimu sana na kumbe sio wa muhimu, anajidanganya mwenyewe. Kila mmoja aipime kazi yake mwenyewe kuona ikiwa kuna chochote cha kujivunia. Kama ndivyo, uyatunze hayo moyoni mwako wala usijilinganishe na mtu mwingine yeyote. Maana sisi sote tunawajibika kwa yale tunayofanya. Yule anayefundishwa neno la Mungu anapaswa kumshirikisha mwalimu wake mambo mema aliyonayo. Ikiwa mnadhani mnaweza kumdanganya Mungu, mtakuwa mnajidanganya wenyewe. Mtavuna yale mnayopanda. Yule anayepanda kwa kuiridhisha nafsi yake ya dhambi, mavuno yatakayopatikana ni uharibifu kabisa. Lakini mkipanda kwa kuiridhisha Roho, mavuno yenu katika Roho yatakuwa uzima wa milele. Hatupaswi kuchoka katika kutenda mema. Tutapata mavuno yetu kwa wakati sahihi, tusipokata tamaa. Tunapokuwa na nafasi ya kumtendea mema kila mtu, tufanye hivyo. Lakini tuzingatie zaidi kuwatendea mema wale walio wa familia ya waamini. Huu ni mwandiko wa mkono wangu mwenyewe. Mnaweza kuona jinsi herufi zilivyo kubwa. Watu wale wanaojaribu kuwalazimisha ninyi kutahiriwa wanafanya hivyo ili wawaridhishe Wayahudi wenzao. Wanaogopa wasije wakateswa kwa sababu ya msalaba wa Kristo. Maana hata wale waliotahiriwa hawaitii sheria. Na bado wanawataka ninyi mtahiriwe ili waweze kujisifu kwa ajili ya yale waliyowatendea ninyi. Mimi nisijisifu kwa ajili ya mambo kama haya. Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo sababu pekee ya kujivuna kwangu. Kupitia kifo cha Yesu msalabani ulimwengu ukafa kwangu, nami nimeufia ulimwengu. Haijalishi kwamba mtu ametahiriwa au hajatahiriwa. Kinachojalisha ni uumbaji mpya wa Mungu katika Kristo. Amani iwe kwa wale wote wanaoifuata njia hii mpya. Na rehema za Mungu ziwe juu ya watu wake Israeli. Kwa hiyo msinitaabishe kwa namna yoyote. Nina makovu mwilini mwangu yanayoonyesha kuwa mimi ni wa Yesu. Ndugu na dada zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amina. Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu. Mimi ni mtume kwa sababu Mungu mwenyewe alitaka. Kwa watakatifu wa Mungu walioko katika mji wa Efeso, waamini walio wa Kristo Yesu. Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi. Sifa kwake Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika Kristo, Mungu ametupa baraka zote za rohoni zilizoko mbinguni. Kwa kuwa anatupenda alituchagua katika Kristo kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu ili tuwe watakatifu wake, tusio na hatia tunaoweza kusimama mbele zake. Aliamua tangu mwanzo kutufanya kuwa watoto wake kupitia Yesu Kristo. Hivi ndivyo Mungu alivyotaka na ilimpendeza yeye kufanya hivyo. Sifa kwake Mungu kwa sababu ya neema yake ya ajabu aliyotupa bure kupitia Kristo anayempenda. Tumewekwa huru katika Kristo kupitia sadaka ya damu yake. Tumesamehewa dhambi kwa sababu ya wingi na ukuu wa neema ya Mungu. Mungu alitupa bure neema hiyo yote, pamoja na hekima na uelewa wote, na ametuwezesha kuujua mpango wake wa siri. Hivi ndivyo Mungu alitaka, na alipanga kuutekeleza kupitia Kristo. Lengo la Mungu lilikuwa kuukamilisha mpango wake muda sahihi utakapofika. Alipanga kuwa vitu vyote vilivyoko mbinguni na duniani viunganishwe pamoja na Kristo kama kichwa. Tulichaguliwa katika Kristo ili tuwe milki ya Mungu. Mungu alikwisha panga ili tuwe watu wake, kwa sababu ndivyo alivyotaka. Na ndiye ambaye hufanya kila kitu kifanyike kulingana na utashi na maamuzi yake. Sisi Wayahudi ndiyo tuliokuwa wa kwanza kutumaini katika Kristo. Na tulichaguliwa ili tuweze kumletea sifa Mungu katika utukufu wake wote. Ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi. Mliusikia ujumbe wa kweli, yaani Habari Njema kuhusu namna ambavyo Mungu anavyowaokoa. Mlipoisikia Habari Njema hiyo, mkamwamini Kristo. Na katika Kristo, Mungu aliwatia alama maalum kwa kuwapa Roho Mtakatifu aliyeahidi. Roho ni malipo ya kwanza yanayothibitisha kuwa Mungu atawapa watu wake kila kitu alichonacho kwa ajili yao. Sisi sote tutaufurahia uhuru kamili uliowekwa tayari kwa ajili ya walio wake. Na hili litamletea Mungu sifa katika utukufu wake wote. Ndiyo sababu daima ninawakumbuka katika maombi yangu na ninamshukuru Mungu kwa ajili yenu. Nimekuwa nikifanya hivi tangu niliposikia kuhusu imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watu wote wa Mungu. *** Daima ninamwomba Baba aliye mkuu na mwenye utukufu, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ninaomba awape Roho anakayewawezesha kuijua kweli kuhusu Mungu na awasaidie kuzielewa kweli hizo ili mweze kumjua vyema. Ninaomba Mungu afungue mioyo yenu ili mwone kweli yake. Kisha mtalijua tumaini alilochagua kwa ajili yetu. Mtajua kuwa baraka ambazo Mungu amewaahidi watu wake ni nyingi na zimejaa utukufu. Na mtajua kuwa uweza wa Mungu ni mkuu sana kwetu sisi tunaoamini. Ni sawa na nguvu zake kuu alizotumia kumfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumweka akae upande wa kulia wa kiti chake cha enzi huko mbinguni. Amemweka Kristo juu ya watawala wote, mamlaka zote, nguvu zote na wafalme wote. Amempa mamlaka juu ya kila kitu chenye nguvu katika ulimwengu huu na ujao. Mungu alikiweka kila kitu chini ya nguvu za Kristo na kumfanya kuwa kichwa cha kila kitu kwa manufaa ya kanisa. Kanisa ndiyo mwili wa Kristo, yeye ndiye amejaa ndani ya kanisa. Anakikamilisha kila kitu katika kila namna. Zamani mlikuwa wafu kiroho kwa sababu ya dhambi na mambo mliyotenda kinyume na Mungu. Ndiyo, zamani maisha yenu yalijaa dhambi hizo. Mliishi kwa namna ya ulimwengu; mkimfuata mkuu wa nguvu za uovu zilizo katika anga, roho hiyo hiyo inatenda kazi sasa ndani ya watu wasiomtii Mungu. Tuliishi hivyo zamani, tukijaribu kuzifurahisha tamaa zetu za mwili. Tulitenda mambo ambayo miili na akili zetu zilitaka. Kama ilivyo kwa kila mtu ulimwenguni, tulistahili kuteseka kutokana na hasira ya Mungu kwa sababu ya jinsi tulivyokuwa. Lakini Mungu ni mwingi wa rehema na anatupenda sana. Tulikuwa wafu kiroho kwa sababu ya matendo maovu tuliyotenda kinyume naye. Lakini yeye alitupa maisha mapya pamoja na Kristo. (Mmeokolewa na neema ya Mungu.) Ndiyo, ni kwa sababu sisi ni sehemu ya Kristo Yesu, ndiyo maana Mungu alitufufua pamoja naye kutoka kwa wafu na akatuketisha pamoja naye mbinguni. Mungu alifanya hivi ili wema wake kwetu sisi tulio wa Kristo Yesu uweze kuonesha nyakati zote zijazo utajiri wa ajabu wa neema yake. Nina maana ya kuwa mmeokolewa kwa neema kwa sababu mliweka imani yenu kwake. Hamkujiokoa ninyi wenyewe; bali ni zawadi kutoka kwa Mungu. Msijisifu kwa kuwa hamkuokolewa kutokana na matendo yenu. Mungu ndiye aliyetufanya hivi tulivyo. Ametuumba wapya katika Kristo Yesu ili tutende mambo mema katika maisha yetu. Mambo aliyokwisha kutupangia. Hamkuzaliwa mkiwa Wayahudi. Ninyi ni watu ambao Wayahudi huwaita “Wasiotahiriwa”, na wao wakijiita “Waliotahiriwa” (Tohara yao ni ile inayofanyika kwenye miili yao kwa mikono ya binadamu.) Kumbukeni ya kwamba zamani hamkuwa na Kristo. Hamkuwa raia wa Israeli na hamkujua kuhusu mapatano ya maagano ambayo Mungu aliyaweka kwa watu wake. Hamkuwa na tumaini na hamkumjua Mungu. Lakini sasa mmeungana na Kristo Yesu. Ndiyo, wakati fulani hapo zamani mlikuwa mbali na Mungu, lakini sasa mmeletwa karibu naye kupitia sadaka ya damu ya Kristo. Kristo ndiye sababu ya amani yetu. Yeye ndiye aliyetufanya sisi Wayahudi nanyi msio Wayahudi kuwa wamoja. Tulitenganishwa na ukuta wa chuki uliokuwa kati yetu, lakini Kristo aliubomoa. Kwa kuutoa mwili wake mwenyewe, Kristo aliisitisha sheria pamoja na kanuni na amri zake nyingi. Kusudi lake lilikuwa ni kuyafanya makundi mawili yawe wanadamu wamoja waliounganishwa naye. Kwa kufanya hivi alikuwa analeta amani. Kupitia msalaba Kristo alisitisha uhasama kati ya makundi mawili. Na baada ya makundi haya kuwa mwili mmoja, alitaka kuwapatanisha wote tena kwa Mungu. Alifanya hivi kwa kifo chake msalabani. Kristo alikuja na kuwaletea ujumbe wa amani ninyi msio Wayahudi mliokuwa mbali na Mungu. Na aliwaletea pia ujumbe huo wa amani watu waliokaribu na Mungu. Ndiyo, kupitia Kristo sisi sote tuna haki ya kumjia Baba katika Roho mmoja. Hivyo ninyi msio Wayahudi si wageni wala wahamiaji, lakini ninyi ni raia pamoja na watakatifu wa Mungu. Ninyi ni wa familia ya Mungu. Ninyi mnaoamini ni kama jengo linalomilikiwa na Mungu. Jengo hilo limejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii. Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la muhimu sana katika jengo hilo. Jengo lote limeunganishwa katika Kristo, naye hulikuza na kuwa hekalu takatifu katika Bwana. Na katika Kristo mnajengwa pamoja na watu wake wengine. Mnafanywa kuwa makazi ambapo Mungu anaishi katika Roho. Hivyo, mimi Paulo ni mfungwa kwa sababu ninamtumikia Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi msio Wayahudi. Mnajua hakika ya kuwa Mungu alinipa kazi hii kupitia neema yake ili niwasaidie. Mungu alinionyesha na nikaweza kuujua mpango wake wa siri. Nimekwisha kuandika kiasi fulani juu ya hili. Na ikiwa mtasoma nilichowaandikia, mtajua kuwa ninaielewa siri ya kweli kuhusu Kristo. Watu walioishi zamani hawakuambiwa siri hiyo. Lakini sasa, kupitia Roho, Mungu amewawezesha mitume na manabii wake watakatifu kuijua siri hiyo. Na siri hiyo ni hii: Kwa kuikubali Habari Njema, wale wasio Wayahudi watashiriki pamoja na Wayahudi katika baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake. Wao ni sehemu ya mwili mmoja, na wanashiriki manufaa ya ahadi ambayo Mungu aliitimiza kupitia Kristo Yesu. Kwa kipawa cha neema ya Mungu, nilifanywa mtumishi wa kuihubiri Habari Njema. Alinipa neema hiyo kwa nguvu zake. Mimi nisiye na umuhimu zaidi miongoni mwa watu wa Mungu. Lakini alinipa kipawa hiki cha kuwahubiri wasio Wayahudi Habari Njema kuhusu utajiri alionao Kristo. Utajiri huu ni mkuu na si rahisi kuuelewa kikamilifu. Pia Mungu alinipa kazi ya kuwaambia watu kuhusu mpango wa siri yake ya kweli. Aliificha siri hii ya kweli ndani yake tangu mwanzo wa nyakati. Ndiye aliyeumba kila kitu. Lengo lake lilikuwa kwamba watawala wote na mamlaka zote zilizo mbinguni zijue njia nyingi anazotumia kuionesha hekima yake. Watalijua hili kwa sababu ya kanisa. Hii inaendana na mpango aliokuwa nao Mungu tangu mwanzo wa nyakati. Alitekeleza mpango wake kupitia Kristo Yesu Bwana wetu. Kwa kuwa tu wake Kristo tunakuja mbele za Mungu tukiwa huru bila woga. Tunaweza kufanya hivi kwa sababu ya uaminifu wake Kristo. Hivyo ninawaomba msikate tamaa kutokana na yale yanayonipata. Mateso yangu ni faida kwenu, na pia ni kwa ajili ya heshima na utukufu wenu. Hivyo ninapiga magoti nikimwomba Baba. Ambaye katika yeye kila familia iliyoko mbinguni na duniani inapewa jina. Ninamwomba Baba kwa kadri ya utajiri wa utukufu wake awajaze nguvu za ndani kwa nguvu za Roho wake. Ninaomba kwamba Kristo aishi katika mioyo yenu kwa sababu ya imani yenu. Ninaomba maisha yenu yawe na mizizi mirefu na misingi imara katika upendo. Na ninaomba ili ninyi na watakatifu wote wa Mungu muwe na uwezo wa kuuelewa upana, urefu, kimo na kina cha ukuu wa upendo wa Kristo. Upendo wa Kristo ni mkuu kuliko namna ambavyo mtu yeyote anaweza kujua, lakini ninawaombea ili mweze kuujua. Ndipo mtajazwa kwa kila kitu alichonacho Mungu kwa ajili yenu. Tukiwa na nguvu za Mungu zinazotenda kazi ndani yetu, anaweza kufanya zaidi, zaidi ya kila kitu tunachoweza kuomba au kufikiri. Atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kila wakati, milele na milele. Amina. Hivyo, mimi niliye mfungwa kwa ajili ya Bwana nawasihi mwishi kwa jinsi inavyowapasa watu wa Mungu, kwa sababu aliwachagua muwe wake. Iweni wanyenyekevu na wapole siku zote. Mvumiliane na kuchukuliana ninyi kwa ninyi katika upendo. Mmeunganishwa pamoja kwa amani na Roho. Jitahidini mwezavyo kudumu kuutunza umoja huo, mkiunganishwa pamoja kwa amani. Kuna mwili mmoja na Roho moja, na Mungu aliwachagua ili muwe na tumaini moja. Kuna Bwana mmoja, imani moja, na ubatizo mmoja. Mungu ni mmoja na ni Baba wetu sote, anayetawala juu ya kila mtu. Hutenda kazi kupitia kwetu sote na ndani yetu sote. Kristo alimpa kila mmoja wetu karama. Kila mmoja alipokea kwa jinsi alivyopenda yeye kuwapa. Ndiyo maana Maandiko yanasema, “Alipaa kwenda mahali pa juu sana; aliwachukua wafungwa pamoja naye, na akawapa watu vipawa.” Inaposema, “Alipaa juu,” inamaanisha nini? Inamaanisha kuwa kwanza alikuja chini duniani. Hivyo Kristo alishuka chini, na ndiye aliyekwenda juu. Alikwenda juu ya mbingu za juu zaidi ili avijaze vitu vyote pamoja naye. Na Kristo huyo huyo aliwapa watu hawa vipawa: aliwafanya wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kwenda na kuhubiri Habari Njema, na wengine kuwa wachungaji ili wawafundishe watu wa Mungu. Mungu aliwapa hao ili kuwaandaa watakatifu wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma, kuufanya imara mwili wa Kristo. Kazi hii inabidi iendelee hadi wote tutakapounganishwa pamoja katika lile tunaloliamini na tunalolijua kuhusu Mwana wa Mungu. Lengo letu ni kufanana na mtu mzima aliyekomaa na kuwa kama Kristo tukiufikia ukamilifu wake wote. Ndipo tutakapokuwa si kama watoto wachanga. Hatutakuwa watu ambao nyakati zote hubadilika kama meli inayochukuliwa na mawimbi huku na kule. Hatutaweza kuathiriwa na fundisho lolote jipya tutakalosikia kutoka kwa watu wanaojaribu kutudanganya. Hao ni wale wanaoweka mipango ya ujanja na kutumia kila aina ya mbinu kuwadanganya wengine waifuate njia iliyopotoka. Hapana, tunapaswa kusema ukweli kwa upendo. Tutakua na kuwa kama Kristo katika kila njia. Yeye ni kichwa, na mwili wote unamtegemea yeye. Viungo vyote vya mwili vimeunganishwa na kushikanishwa pamoja, huku kila kiungo kikitenda kazi yake. Hili huufanya mwili wote ukue na kujengeka katika upendo. Nina kitu cha kuwaambia kutoka kwa Bwana. Ninawaonya: Msiendelee kuishi kama wale wasiomwamini Mungu wetu. Mawazo yao hayafai kitu. Hawana ufahamu, na hawajui lolote kwa sababu wamekataa kusikiliza. Hivyo hawawezi kupata maisha mapya Mungu anayowapa watu. Wamepoteza hisia zao za aibu na wanayatumia maisha yao kutenda yale yaliyo mabaya kimaadili. Zaidi ya hapo wanataka kutenda kila aina ya uovu. Lakini aina hiyo ya maisha haiko kama ile mliyojifunza mlipomjua Kristo. Najua kwamba mlisikia juu yake, na ndani yake mlifundishwa ukweli. Ndiyo, ukweli umo ndani ya Yesu. Mlifundishwa kuacha utu wenu wa kale. Hii inamaanisha kwamba mnapaswa kuacha kuishi katika njia za uovu mlivyoishi zamani. Utu wenu wa kale huharibika zaidi na zaidi, kwa sababu watu hudanganywa na uovu wanaotaka kuutenda. Mnapaswa kufanywa upya katika mioyo yenu na katika fikra zenu. Kila mmoja wenu auvae utu ule mpya ulioumbwa kwa kufananishwa na Mungu, ambao kwa hakika una wema na ni wenye kumpendeza Mungu. Hivyo mnapaswa kuacha kusema uongo, “Nyakati zote mseme ukweli tu,” kwa sababu wote sisi tunahusiana na ni wa mwili mmoja. “Unapokasirika, usiruhusu hasira hiyo ikusababishe wewe kutenda dhambi,” na usiendelee na hasira kwa siku nzima. Usimwachie Ibilisi nafasi ya kukushinda. Yeyote ambaye amekuwa akiiba anapaswa kuacha kuiba na afanye kazi. Unapaswa kutumia mikono yako kufanya kitu chenye kufaa. Hapo utakuwa na kitu cha kuwashirikisha walio maskini. Unapozungumza, usiseme chochote kilicho kibaya. Bali useme mambo mazuri ambayo watu wanayahitaji ili waimarike. Ndipo kile unachosema kitakuwa ni baraka kwa wale wanaokusikia. Tena usimhuzunishe Roho Mtakatifu. Mungu alikupa Roho Mtakatifu kama uthibitisho kwamba wewe ni wake na kwamba atakulinda hadi siku atakapokufanya uwe huru kabisa. Usiwe na uchungu, wala kukasirika. Kamwe usiongee kwa hasira au kusema chochote ili uwaumize wengine. Usifanye chochote kilicho kiovu. Mwe mwema na mpendane ninyi kwa ninyi. Msameheane ninyi kwa ninyi kama Mungu alivyowasamehe ninyi kwa njia ya Kristo. Ninyi ni watoto wa Mungu wapendwao, hivyo jitahidini kuwa kama yeye. Ishini maisha ya upendo. Wapendeni wengine kama Kristo alivyotupenda sisi. Alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu na kuwa sadaka ya harufu ya manukato mazuri na dhabihu kwa Mungu. Lakini hakupaswi kuwepo dhambi ya zinaa kati yenu. Hakupaswi kuwepo aina yoyote ya uasherati au matamanio ya zinaa, kwa sababu mambo kama hayo hayastahili kwa watakatifu wa Mungu. Vivyo hivyo, pasiwepo na mazungumzo maovu miongoni mwenu. Msizungumze mambo ya kipuuzi au ya uchafu. Hayo siyo kwa ajili yenu. Bali mnatakiwa kutoa shukrani kwa Mungu. Mnaweza kuwa na uhakika wa hili: Hakuna atakayepata sehemu katika ufalme wa Kristo na wa Mungu kama mtu huyo atakuwa anafanya dhambi ya uzinzi, au akitenda mambo maovu, au kama atakuwa mtu wa kutamani vitu zaidi na zaidi. Mtu mwenye choyo kama huyo atakuwa anamtumikia mungu wa uongo. Msimruhusu mtu yeyote awadanganye kwa maneno yasiyo ya kweli. Mungu huwakasirikia sana watu wasipomtii kama hivyo. Hivyo msiwe na jambo lolote pamoja nao. Hapo zamani mlijaa giza, lakini sasa mmejaa nuru katika Bwana. Hivyo ishini kama watoto wa nuru. Nuru hii huleta kila aina ya wema, maisha ya haki, na kweli. Jaribuni kutafuta yale yanayompendeza Bwana. Msishiriki katika mambo yanayotendwa na watu wa giza, yasiyosababisha jambo lolote zuri. Badala yake, mwambieni kila mtu jinsi mambo hayo yasivyokuwa sahihi. Hakika, ni aibu hata kuyazungumzia mambo haya wanayoyatenda sirini. Lakini nuru inaonesha wazi jinsi mambo hayo yasivyokuwa sahihi. Ndiyo, kila kitu kinawekwa wazi na nuru. Ndiyo maana tunasema, “Amka, wewe unayelala! Fufuka kutoka kwa wafu, na Kristo atakuangazia nuru yake.” Hivyo, muwe makini sana jinsi mnavyoishi. Ishini kwa busara, si kama wajinga. Nasema kwamba jitahidini kutumia kila fursa mliyo nayo katika kutenda mema, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. Hivyo msiwe kama wajinga katika maisha yenu, bali mfahamu yale ambayo Bwana anapenda ninyi mfanye. Msilewe kwa mvinyo, ambao utaharibu maisha yenu, bali mjazwe Roho. Mhimizane ninyi kwa ninyi katika zaburi, nyimbo za sifa, na nyimbo zinazoongozwa na Roho. Imbeni na msifuni Bwana katika mioyo yenu. Siku zote mshukuruni Mungu Baba kwa mambo yote katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Mwe radhi kuhudumiana ninyi kwa ninyi kwa kuwa mnamheshimu Kristo. Wake, muwe radhi kuwahudumia waume zenu kama mlivyo radhi kumtumikia Bwana. Mume ni kichwa cha mke wake, kama Kristo alivyo kichwa cha kanisa. Kristo ni Mwokozi wa kanisa, ambalo ni mwili wake. Kanisa hutumika chini ya Kristo, hivyo ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi wake. Mnapaswa kuwa radhi kuwahudumia waume zenu katika kila jambo. Waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa na kuyatoa maisha yake kwa ajili yake. Alikufa ili alitakase kanisa lake. Alitumia ujumbe wa Habari Njema kulisafisha kanisa kwa kuliosha katika maji. Kristo alikufa ili aweze kujiletea mwenyewe kanisa lililo kama bibi harusi katika uzuri wake wote. Alikufa ili kanisa liweze kuwa takatifu na lisilo na dosari, lisilokuwa na uovu au dhambi au chochote kilicho kibaya ndani yake. Na waume wawapende hivyo wake zao. Wawapende wake zao kama vile ni miili yao wenyewe. Mtu anayempenda mkewe anajipenda mwenyewe, kwa sababu kamwe hakuna anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza. Na hivyo ndivyo Kristo anavyolifanyia kanisa kwa sababu sisi sote ni viungo vya mwili wake. Maandiko yanasema, “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake na kuungana na mkewe, nao hao wawili watafanyika mwili mmoja.” Siri hiyo ya kweli ni ya muhimu sana, ninazungumza juu ya Kristo na kanisa. Lakini kila mmoja wenu anapaswa kumpenda mkewe kama anavyojipenda mwenyewe. Na mke anapaswa kumheshimu mume wake. Watoto, watiini wazazi wenu katika namna ambayo Bwana anataka, kwa sababu hili ni jambo sahihi kutenda. Amri husema, “Waheshimu baba yako na mama yako.” Hii ndiyo amri ya kwanza iliyo na ahadi pamoja nayo. Na hii ndiyo ahadi: “Ndipo utakapofanikiwa, na utakuwa na maisha marefu duniani.” Wababa, msiwakasirishe watoto wenu, lakini waleeni kwa mafunzo na mausia mliyopokea kutoka kwa Bwana. Watumwa, watiini bwana zenu hapa duniani kwa hofu na heshima. Na fanyeni hivi kwa moyo ulio wa kweli, kama mnavyomtii Kristo. Mfanye hivi siyo tu kwa kuwafurahisha bwana zenu wakati wanapowaona, bali wakati wote. Kwa vile ninyi hakika ni watumwa wa Kristo, mfanye kwa mioyo yenu yale Mungu anayotaka. Fanyeni kazi zenu, na mfurahie kuzifanya. Fanyeni kana kwamba mnamtumikia Bwana, siyo tu bwana wa duniani. Kumbukeni kwamba Bwana atampa kila mmoja zawadi kwa kufanya vema. Kila mmoja, mtumwa au aliye huru, atapata zawadi kwa mambo mema aliyotenda. Mabwana, kwa jinsi hiyo hiyo, muwe wema kwa watumwa wenu. Msiseme mambo ya kuwatisha. Mnajua kuwa yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, na humchukulia kila mmoja sawa. Hapa lipo neno moja la mwisho la ushauri: Mtegemeeni Bwana kwa ajili ya nguvu zenu. Wekeni matumaini yenu katika nguvu zake kuu. Vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kupigana dhidi ya hila za Shetani. Mapigano yetu si juu ya watu duniani. Tunapigana dhidi ya watawala, mamlaka na nguvu za giza za ulimwengu huu. Tunapigana dhidi ya nguvu za uovu katika ulimwengu wa roho. Ndiyo sababu mnahitaji silaha zote za Mungu. Ili siku ya uovu, mweze kusimama imara. Na mtakapomaliza mapigano yote, mtaendelea kusimama. Hivyo simameni imara mkiwa mmefungwa mkanda wa kweli viunoni mwenu, na katika vifua vyenu mkiwa mmevaa kinga ya maisha ya haki. Miguuni mwenu vaeni Habari Njema za amani ili ziwasaidie msimame imara. Pia itumieni ngao ya imani ambayo itatumika kuizuia mishale inayowaka moto inayotoka kwa yule Mwovu. Upokeeni wokovu wa Mungu kama chapeo yenu. Na chukueni upanga wa Roho, yaani mafundisho ya Mungu. Ombeni katika Roho kila wakati. Ombeni maombi ya aina zote, na ombeni kila mnachohitaji. Ili mfanye hivi ni lazima muwe tayari. Msikate tamaa. Waombeeni watu wa Mungu daima. Pia ombeni kwa ajili yangu ili ninapoongea, Mungu anipe maneno ili niweze kusema siri ya kweli juu ya Habari Njema bila woga. Ninayo kazi ya kuhubiri Habari Njema, na hicho ndicho ninachofanya sasa humu gerezani. Niombeeni ili ninapowahubiri watu Habari Njema, nihubiri kwa ujasiri kama inavyonipasa kuhubiri. Namtuma kwenu Tikiko, ndugu yetu mpendwa na msaidizi mwaminifu katika kazi ya Bwana. Atawaeleza kila kitu kinachonipata. Kisha mtaelewa jinsi nilivyo na ninachofanya. Ndiyo sababu namtuma yeye ili awajulishe hali zetu na tuwatie moyo. Namwomba Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo awape amani, upendo na imani ndugu zangu wote mlio huko. Naomba neema ya Mungu iwe pamoja nanyi nyote mnaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa pendo lisilo na mwisho. Salamu kutoka kwa Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu. Kwenu ninyi nyote, watakatifu wa Mungu mlioko Filipi, mlio wa Kristo Yesu, wakiwemo wazee na mashemasi wenu. Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu, Bwana wetu, iwe pamoja nanyi. Ninamshukuru Mungu kila wakati ninapowakumbuka. Kila wakati ninapowaombea ninyi nyote, daima ninawaombea kwa furaha. Ninamshukuru Mungu kwa namna mlivyonisaidia nilipokuwa ninawahubiri watu Habari Njema. Mlinisaidia tangu siku ya kwanza mlipoamini mpaka sasa. Nina uhakika kwamba Mungu, aliyeianzisha kazi njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka itakapomalizika siku ile ambayo Kristo Yesu atakuja tena. Ninajua niko sahihi kwa namna ile ninayowawazia ninyi nyote kwa sababu mko karibu sana na moyo wangu. Mmechangia sehemu muhimu sana katika neema ya Mungu kwa ajili yangu wakati huu nikiwa gerezani, na wakati wowote ninapoutetea na kuuthibitisha ukweli wa Habari njema. Mungu anajua kwamba ninataka sana kuwaona. Ninawapenda nyote kwa upendo wa Kristo Yesu. Hili ndiyo ombi langu kwa ajili yenu: Ya kwamba mkue zaidi na zaidi katika hekima na ufahamu kamili pamoja na upendo; ya kwamba mjue tofauti kati ya kitu kilicho muhimu na kisicho muhimu ili muwe safi msio na lawama, mkiwa tayari kwa siku atakayokuja Kristo; Maisha yenu yajaye matendo mengi mema yanayozalishwa na Kristo Yesu ili kumletea Mungu utukufu na sifa. Ndugu zangu, ninataka mjue kwamba yote yaliyonipata yamesaidia katika kusambaza Habari Njema, ingawa ninyi mnaweza kuwa mlitarajia kinyume chake. Walinzi wote wa Kirumi na wengine wote hapa wanafahamu kuwa nimefungwa kwa sababu ninamtumikia Kristo. Kufungwa kwangu gerezani kumesababisha waamini walio wengi hapa kuweka tumaini lao kwa Bwana, na kuhubiri ujumbe wa Mungu kwa ujasiri mwingi pasipo woga. Baadhi ya watu wanahubiri ujumbe wa Kristo kwa sababu wananionea wivu na wanataka watu wawafuate wao badala yangu. Wengine wanahubiri kwa sababu wanataka kusaidia. Wanahubiri kwa sababu ya upendo. Wanafahamu kuwa Mungu ameniweka humu gerezani ili kuitetea Habari Njema. Lakini wengine wanahubiri kuhusu Kristo kwa sababu wanataka kujikweza wenyewe. Chachu yao si safi. Wanafanya hivi kwa kudhani kuwa itanisababishia uchungu mwingi niwapo gerezani. Lakini hiyo haijalishi. Kitu cha muhimu ni kuwa wanawahubiri watu kuhusu Kristo, wakiwa na chachu safi au isiyo safi. Ninafurahi wanafanya hivyo. Nitaendelea kufurahi, kwa sababu ninajua kwamba kupitia maombi yenu na kipawa cha Roho wa Yesu Kristo mazingira haya magumu hatimaye yataniletea uhuru wangu. Nimejaa tumaini na uhakika, sina sababu yeyote ya kuona haya. Nina uhakika nitaendelea kuwa na ujasiri wa kuhubiri kwa uhuru kama ambavyo nimekuwa. Na Kristo atatukuzwa kwa ninayoyafanya katika mwili wangu, ikiwa nitaishi au nitakufa. Sababu yangu pekee ya kuishi ni kumtumikia Kristo. Kifo kingekuwa bora zaidi. Nikiendelea kuishi hapa ulimwenguni, nitaweza kumfanyia kazi Bwana. Lakini kati ya kufa na kuishi, sijui ningechagua kipi. Ungekuwa uchaguzi mgumu. Ninataka kuyaacha maisha haya ili niwe na Kristo. Hiyo ingekuwa bora zaidi kwangu; hata hivyo, mnanihitaji hapa nikiwa hai. Nina uhakika juu ya hili, hivyo ninajua nitakaa hapa ili niwe nanyi na niwasaidie kukua na kuwa na furaha katika imani yenu. Mtafurahi sana nitakapokuwa hapo pamoja nanyi tena kutokana na kile ambacho Kristo Yesu amefanya ili kunisaidia. Zaidi ya yote, hakikisheni kuwa mnaishi pamoja kama jamii ya watu wa Mungu katika namna inayoiletea heshima Habari Njema kuhusu Kristo. Kisha, ikiwa nitakuja kuwatembelea au ikiwa nitakuwa mbali nanyi na kuyasikia tu mambo kuhusu ninyi, nitajua ya kuwa mmesimama pamoja katika roho moja na kwamba mnafanya kazi pamoja kwa moyo mmoja kama timu moja, katika kuwasaidia wengine kuiamini Habari Njema. Na hamtawaogopa wale walio kinyume nanyi. Imani yenu thabiti itakuwa kama ishara kwao ya kuangamia kwenu. Lakini kwa hakika ni ishara ya wokovu wenu. Na hiki ni kipawa kutoka kwa Mungu. Mungu amewabariki ninyi kwa heshima si ya kumwamini Kristo tu, lakini pia ya kupata mateso kwa ajili yake. Mliyaona magumu mengi niliyokabiliana nayo, na mnasikia kwamba bado nakabiliwa na masumbufu mengi. Ninyi nanyi imewapasa kuyakabili masumbufu hayo pia. Fikirini kuhusu kile ambacho tulichonacho kwa sababu tunamilikiwa na Kristo: hamasa aliyotuletea, faraja ya upendo wake, ushirika katika Roho wake, huruma na wema aliotuonyesha. Ikiwa mnazifurahia baraka hizi, basi fanyeni yale yatakayoikamilisha furaha yangu: iweni na nia moja na mpendane ninyi kwa ninyi. Iweni na umoja katika malengo yenu na katika kufikiri kwenu. Msiruhusu ubinafsi au kiburi viwe dira yenu. Badala yake muwe wanyenyekevu mkiwathamini wengine kuliko ninyi wenyewe. Kila mmoja wenu asijishugulishe kwa mema yake yeye mwenyewe bali kwa mema ya wengine. Hivi ndivyo mnapaswa kufikiri, kuhisi na kutenda katika maisha yenu kwa pamoja, kama vile Kristo Yesu alivyofikiri: Alikuwa sawa na Mungu katika namna zote, lakini hakufikiri kwamba kuwa sawa na Mungu kilikuwa kitu cha manufaa kwake. Badala yake, aliacha kila kitu, hata sehemu yake pamoja na Mungu. Akakubali kuwa kama mtumwa, akiwa katika umbo la binadamu. Wakati wa maisha yake kama mtu, Alijinyenyekeza na akawa mtiifu kabisa kwa Mungu, hata jambo hilo liliposababisha kifo chake msalabani. Hivyo ndiyo sababu Mungu alimpa mahali pa heshima sana, na akampa jina lililo kuu kuliko majina yote. Hivyo kila mtu atasujudu kumheshimu Yesu. Kila mmoja aliye mbinguni, duniani na wale walio chini ya dunia. Wote watakiri kwamba, “Yesu Kristo ni Bwana,” na hili litamtukuza Mungu Baba. Rafiki zangu wapendwa, daima mnatii yale mliyofundishwa. Kama mlivyotii nilipokuwa pamoja nanyi, ni muhimu zaidi na zaidi kwamba mtii wakati huu ambapo sipo pamoja nanyi. Hivyo ni lazima mwendelee kuishi katika namna inayoleta maana kwa wokovu wenu. Fanyeni hivi kwa wingi wa heshima na utii kwa Mungu. Ndiyo, Mungu ndiye anayetenda kazi ndani na miongoni mwenu. Anawasaidia ninyi kutaka kutenda yanayomfurahisha, naye anawapa nguvu ya kuyatenda. Fanyeni mambo yote pasipo kulalamika wala kubishana. Nanyi mtakuwa watoto wa Mungu wasiolaumiwa na wasio na hatia. Ijapokuwa mnaishi mkiwa mmezungukwa na watu wasio waaminifu wasiojali thamani haki. Katikati ya watu hao mnang'ara kama mianga katika ulimwengu wenye giza, nanyi mnawapa mafundisho yanayotoa uhai. Hivyo nitaona fahari juu yenu wakati Kristo atakapokuja tena. Ninyi ndiyo mtakaothibitisha kuwa kazi niliyoifanya haikukosa matokeo, ya kwamba nilishindana mbio na nikashinda. Imani yenu inayatoa maisha yenu kama sadaka katika kumtumikia Mungu. Hata kama ni kweli kwamba sasa ninajimimina mimi mwenyewe kama sadaka ya kinywaji pamoja na sadaka yenu, ninayo furaha, na nitawashirikisha ninyi nyote furaha yangu. Ninyi pia mnapaswa kufurahi na kunishirikisha furaha yenu. Kwa baraka za Bwana Yesu, ninategemea kuwa nitamtuma Timotheo kwenu hivi karibuni. Naye atarejesha kwangu taarifa kuhusu ninyi ili nifurahi. Sina mtu mwingine yeyote kama Timotheo, ambaye kwa dhati kabisa anayajali mambo yanayowahusu. Wengine wote wanajishughulisha na maisha yao wenyewe. Hawajali kazi ya Yesu Kristo. Mnafahamu Timotheo amejithibitisha kuwa ni mtu wa aina gani. Ametumika pamoja nami katika kuhubiri Habari Njema kwa njia ambavyo mwana angemtumikia baba yake. Ninategemea kumtuma aje kwenu haraka baada ya kujua yatakayonipata. Bwana hunifanya niwe jasiri ili niweze pia kuja kwenu haraka. Kwa sasa, nadhani ni lazima nimrudishe Epafrodito kwenu. Ni mtumishi na mtenda kazi pamoja nami na askari mwenzangu katika jeshi la Bwana. Nilipotaka msaada, mlimtuma kwangu. Kama mjumbe wenu, alinihudumia mahitaji yangu. Lakini sasa anataka kuwaona ninyi nyote tena. Ana wasiwasi sana kwa sababu mlisikia kuwa alikuwa mgonjwa. Alikuwa mgonjwa karibu ya kufa. Lakini Mungu alimsaidia yeye na mimi ili nisiwe na huzuni zaidi. Hivyo ninataka sana kumtuma kwenu. Ili mtakapomwona, mfurahi. Nami nitaacha kuwa na wasiwasi juu yenu. Mkaribisheni kwa furaha nyingi katika Bwana. Waheshimuni watu kama Epafrodito. Anapaswa kuheshimiwa kwa sababu alikaribia kufa akifanya kazi kwa ajili ya Kristo. Aliyaweka maisha yake katika hatari ili aweze kunisaidia. Ni msaada ambao msingeweza kunisaidia. Kwa hiyo sasa, kaka na dada zangu, furahini kwa kuwa ninyi ni wa Bwana. Sisiti kuwaandikia mambo haya haya, kwa sababu yatawasaidia ninyi kuwa imara na salama. Mjihadhari na mbwa, mjihadhari na wafanyakazi waovu, mjihadhari na watu wanaotaka kumkata kila mtu ambaye hajatahiriwa. Lakini sisi ndiyo wenye tohara ya kweli, tunaomwabudu Mungu kupitia Roho wake. Hatutumaini katika namna tulivyo kwa kuzaliwa au kwa yale tuliyoyakamilisha. Tunajivuna kuwa sisi ni milki ya Kristo Yesu. Hata kama ninaweza kujitumainisha mimi mwenyewe, bado sifanyi hivyo. Ikiwa kuna watu wanadhani wana sababu za kutumaini sifa za kibinadamu, wanapaswa kujua kuwa nina sababu zaidi za kufanya hivyo. Nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa. Mimi ni Myahudi wa kabila la Benjamini. Mimi ni Mwebrania halisi, hata wazazi wangu pia. Nikawa Farisayo na nilitii torati kwa uangalifu sana. Nilikuwa na hamu sana ya kumridhisha Mungu hata nikalitesa kanisa. Kwa usahihi niliitii sheria ya Musa. Wakati fulani mambo haya yote yalikuwa muhimu kwangu. Lakini kwa sababu ya Kristo, sasa ninayachukulia mambo haya yote kuwa yasiyo na thamani. Na si haya tu, lakini sasa ninaelewa kuwa kila kitu ni hasara tu ukilinganisha na thamani kuu zaidi ya kumjua Kristo Yesu, ambaye sasa ni Bwana wangu. Kwa ajili yake nilipoteza kila kitu. Na ninayachukulia yote kama kinyesi, ili nimpate Kristo. Ninataka niwe wake. Katika Kristo ninayo haki mbele za Mungu, lakini kuwa na haki mbele za Mungu hakuji kwa kuitii sheria, Bali inakuja toka kwa Mungu kupitia imani kwa Kristo. Mungu anatumia imani yangu kwa Kristo kunihesabia haki. Ninachotaka ni kumjua Kristo na nguvu iliyomfufua kutoka kwa wafu. Ninataka kushiriki katika mateso yake na kuwa kama yeye hata katika kifo chake. Kisha mimi mwenyewe naweza kuwa na matumaini kwamba nitafufuliwa kutoka kwa wafu. Sisemi kuwa nimekwisha kupata ujuzi huo au kuifikia shabaha ya mwisho. Lakini bado ninajitahidi kuifikia shabaha kwa kuwa ndivyo ambavyo Kristo Yesu anataka nifanye. Ndiyo sababu alinifanya kuwa wake. Kaka na dada zangu, ninajua ya kuwa bado nina safari ndefu. Lakini kuna kitu kimoja ninachofanya, nacho ni kusahau yaliyopita na kujitahidi kwa kadri ninavyoweza kuyafikia malengo yaliyo mbele yangu. Ninaendelea kupiga mbio kuelekea mwisho wa mashindano ili niweze kushinda tuzo ambayo Mungu ameniitia kutoka mbinguni kwa njia ya Kristo Yesu. Sisi sote tuliokua kiroho tunapaswa kufikiri namna hii. Na ikiwa kuna jambo lolote ambalo hamkubaliani nalo, Mungu atalifunua kwenu. Lakini tunapaswa kuendelea kuifuata kweli tuliyonayo tayari. Kaka na dada zangu, unganeni pamoja na mfuate mfano wangu. Mtazame na mjifunze pia kutoka kwa wale wanaoishi katika namna tuliyoionesha kwenu. Wapo wengi ambao mwenendo wao unaonesha kuwa ni adui za msalaba wa Kristo. Nimekwishawaambia kuhusu hao mara nyingi. Na inanifanya nitokwe machozi ninapowaambia kuhusu watu hao sasa. Wanauendea uharibifu kwa namna wanavyoishi. Wanaabudu tamaa za mili yao kana kwamba hizo ndizo Mungu. Wanatenda mambo ya aibu na wanajivuna kwa kutenda mambo hayo. Wanayawazia mambo ya kidunia tu. Lakini sisi tunatawaliwa na serikali iliyoko mbinguni. Tunamsubiri Mwokozi wetu, Bwana wetu Yesu Kristo atakayekuja kutoka mbinguni. Ataibadilisha miili yetu minyenyekevu na kuifanya iwe kama mwili wake yeye mwenyewe, mwili wenye utukufu. Kristo atafanya hivi kwa nguvu yake inayomwezesha kutawala juu ya vyote. Kaka na dada zangu wapenzi, ninawapenda na ninataka kuwaona. Mnanifurahisha na ninajivuna kwa sababu yenu. Endeleeni kuwa imara kumfuata Bwana kama nilivyowaambia. Ninawasihi Euodia na Sintike, ninyi nyote wawili ni wa Bwana, hivyo muwe na mtazamo mmoja. Kwa ajili ya hili ninamwomba rafiki yangu aliyetumika pamoja nami kwa uaminifu: Wasaidieni wanawake hawa. Waliwahubiri watu Habari Njema kwa bidii kama watendaji wenzangu tukiwa pamoja na Klementi na wengine waliofanya kazi pamoja nami. Majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima. Furahini katika Bwana daima. Ninasema tena, furahini. Kila mtu auone wema na uvumilivu wenu. Bwana yu karibu kuja. Msisumbuke kitu chochote, lakini salini na kumwomba Mungu kwa mahitaji yenu. Mshukuruni Mungu wakati mnapomwomba yale mnayohitaji. Na kwa kuwa ninyi ni milki ya Kristo Yesu, amani ya Mungu itailinda mioyo na mawazo yenu isipate wasiwasi. Amani yake inaweza kutenda haya zaidi ya akili za kibinadamu. Na sasa, mwisho kabisa, kaka na dada zangu, fikirini kuhusu yale yaliyo ya kweli, ya kuheshimiwa, ya haki, yaliyo safi, yenye kupendeza, na yanayosemwa vema. Yatendeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu, niliyowaambia na yale mliyoyaona nikitenda. Na Mungu atoaye amani atakuwa pamoja nanyi. Nimefurahi sana katika Bwana kwa sababu mmeonesha tena kuwa mnanijali. Mmeendelea kujali juu yangu, lakini haikuwepo njia ya kuonesha hili. Ninawaambia hili, si kwa sababu ninahitaji msaada kutoka kwa yeyote. Nimejifunza kuridhika na kile nilichonacho na chochote kinachotokea. Ninajua namna ya kuishi ninapokuwa na vichache na ninapokuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuishi katika hali zote, ninapokuwa na vyakula vingi au ninapokuwa na njaa, ninapokuwa na vingi zaidi ya ninavyohitaji au ninapokuwa sina kitu. Kristo ndiye anayenitia nguvu kuyakabili mazingira yote katika maisha. Lakini mlifanya vyema mliposhiriki nami katika kipindi changu kigumu. Enyi watu wa Filipi kumbukeni nilipokuja mara ya kwanza kuwahubiri Habari Njema watu wa Makedonia. Nilipoondoka huko, ninyi ndiyo kanisa pekee ambalo lilishirikiana nami katika uhusiano ulioendelea wa kutoa na kupokea. Ukweli ni kuwa hata nilipokuwa Thesalonike, zaidi ya mara moja mlinitumia kila kitu nilichohitaji. Si kwamba natafuta msaada wa kifedha kutoka kwenu. Bali ninataka ninyi mpokee manufaa yanayozidi kukua yanayotokana na kutoa. Nina kila kitu ninachohitaji. Nina zaidi ya hata ninavyohitaji kwa sababu Epafrodito ameniletea kila kitu mlichompa aniletee. Zawadi zenu ni kama sadaka yenye harufu nzuri inayotolewa kwa Mungu. Ni sadaka anayoikubali, na inampendeza. Mungu wangu atatumia utajiri wake wenye utukufu kuwapa ninyi kila kitu mnachohitaji kupitia Kristo Yesu. Utukufu kwa Mungu na Baba yetu milele na milele. Amina. Wasalimuni watakatifu wote wa Mungu walio wake Kristo Yesu. Wale walio katika familia ya Mungu walio pamoja nami wanawasalimu. Na watu wote wa Mungu walio hapa wanawasalimu, hasa wale walio katika utumishi wa Kaisari. Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na utu wenu wa ndani. Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu. Mimi ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alivyotaka niwe. Salamu pia kutoka kwa Timotheo ndugu yetu katika Kristo. Salamu kwenu kaka na dada zetu watakatifu na walio waaminifu katika Kristo mlioko Kolosai. Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu ziwe pamoja nanyi. Katika maombi yetu tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Yeye ndiye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Nasi tunamshukuru Yeye kwa sababu tumesikia kuhusu imani yenu katika Kristo Yesu na upendo wenu kwa watu wa Mungu wote. Imani yenu na upendo wenu vinatokana na ufahamu kwamba mtapokea kile mnachotumaini. Hicho ambacho Mungu amekihifadhi salama mbinguni kwa ajili yenu. Hilo ni tumaini lile lile ambalo mmekuwa nalo tangu mliposikia kwa mara ya kwanza ujumbe wa kweli, yaani Habari Njema. Habari Njema hii imezaa matunda na imeenea ulimwenguni kote. Na hicho ndicho kilichokuwa kikitokea tangu siku mliposikia kwa mara ya kwanza na kuelewa ukweli wa neema ya Mungu. Kweli hiyo mliisikia kutoka kwa Epafra, aliye mtumwa wa Bwana pamoja nasi. Yeye anatusaidia sisi kama mtumishi mwaminifu wa Kristo. Naye ametueleza pia kuhusu upendo mlioupokea kutoka kwa Roho Mtakatifu. Ndugu zangu tangu siku tuliposikia mambo haya juu yenu, tumeendelea kuwaombea, na haya ndiyo maombi yetu kwa ajili yenu: Kwamba Mungu awajaze ufahamu wa mapenzi yake kwa kuwapa hekima na ufahamu wote wa kiroho mnaohitaji; ili hayo yawasaidie kuishi maisha yanayomletea Bwana heshima na kumpendeza yeye katika hali zote; ili maisha yenu yazae matunda mema ya aina mbalimbali na mpate kuongezeka katika maarifa yenu ya Mungu; ili Mungu mwenyewe awaimarishe kwa uwezo wake mkuu, ili muwe na uvumilivu pasipo kukata tamaa mnapokutana na shida. Ndipo nanyi mtakapofurahi, na kumshukuru Mungu Baba. Kwani yeye amewastahilisha kupokea kile alichowaahidi watakatifu wake, wanaoishi katika nuru. Mungu ametuweka huru kutoka katika nguvu za giza. Naye ametuingiza katika ufalme wa Mwanaye mpendwa. Na huyo Mwana amelipa gharama ya kutuweka huru, kwani ndani yake tuna msamaha wa dhambi zetu. Hakuna anayeweza kumwona Mungu, lakini Mwana anafanana kabisa na Mungu. Anatawala juu ya kila kitu kilichoumbwa. Kwa uweza wake, vitu vyote viliumbwa: vitu vya angani na ardhini, vinavyoonekana na visivyoonekana, watawala wote wa kiroho, wakuu, enzi, na mamlaka. Kila kitu kiliumbwa kupitia Yeye na kwa ajili yake. Mwana alikuwapo kabla ya kuumbwa kitu chochote, na vyote vinaendelea kuwepo kwa sababu yake. Yeye ni kichwa cha mwili, yaani kanisa. Yeye ni mwanzo wa maisha yajayo, ni wa kwanza miongoni mwa wote watakaofufuliwa kutoka kwa wafu. Hivyo katika mambo yote yeye ni mkuu zaidi. Mungu alipendezwa kwamba ukamilifu wa uungu wake uishi ndani ya Mwana. Na kupitia Yeye, Mungu alifurahi kuvipatanisha tena vitu vyote kwake Yeye mwenyewe; vilivyoko mbinguni na vilivyoko duniani. Mungu alileta amani kupitia sadaka ya damu ya Mwanaye msalabani. Hapo mwanzo mlitengwa na Mungu, na mlikuwa adui zake katika fikra zenu, kwa sababu ya maovu mliyotenda kinyume naye. Lakini sasa amewafanya kuwa marafiki zake tena, kupitia kifo cha Kristo katika mwili wake. Ili kwa njia hiyo awalete kwake mkiwa watakatifu, msio na lawama na msiohukumiwa jambo lolote mbele zake; na hiki ndicho kitatokea mkiendelea kuiamini Habari Njema mliyoisikia. Mwendelee kuwa imara na kudumu katika imani. Jambo lolote lisiwafanye mkaliacha tumaini lenu mlilopokea mlipoisikia Habari Njema. Habari Njema ile ile ambayo imehubiriwa kwa kila mtu duniani, ndiyo kazi ambayo mimi, Paulo, nilipewa kufanya. Nina furaha kwa sababu ya mateso ninayopata kwa manufaa yenu. Yapo mambo mengi ambayo kupitia hayo Kristo bado anateseka. Nami ninayapokea mateso haya kwa furaha katika mwili wangu kwa ajili ya mwili wake, yaani Kanisa. Nilifanyika kuwa mtumishi wa kanisa kwa sababu Mungu alinipa kazi maalum ya kufanya. Kazi hii inawasaidia ninyi, nayo ni kuuhubiri ujumbe kamili wa Mungu. Ujumbe huu ni ukweli wenye siri uliofichwa tangu mwanzo wa nyakati. Nao ulifichwa kutoka kwa kila mtu kwa muda mrefu, lakini sasa umedhihirishwa kwa watakatifu wa Mungu. Mungu aliamua kuwajulisha watu wake namna Kweli hii ilivyo na utajiri na utukufu. Siri hii ya kweli hii, ambayo ni kwa ajili ya watu wote, ni kwamba Kristo anaishi ndani yenu. Yeye ndiye tumaini la kushiriki katika utukufu wake. Hivyo tunaendelea kuwaambia watu juu ya Kristo. Tunatumia hekima yote kumshauri na kumfundisha kila mtu. Tunajaribu kumleta kila mtu mbele za Mungu kama watu waliokomaa kiroho katika uhusiano wao na Kristo. Kwa kufanya hivi, ninafanya kazi kwa bidii, nikijitahidi na kutumia nguvu kubwa aliyonipa Kristo. Nguvu hiyo inafanya kazi katika maisha yangu. Ninataka mfahamu ni kwa kiwango gani ninawajali ninyi pamoja na ndugu waishio Laodikia na wengine ambao hawajawahi kuniona. Ninataka ninyi nyote pamoja na wao mtiwe moyo na kuunganishwa pamoja katika upendo na kupata uhakika unaoletwa kwa kuielewa ile kweli. Pia, ninataka waijue kweli iliyokuwa siri ambayo sasa imefunuliwa na Mungu. Kweli hiyo ni Kristo mwenyewe. Yeye peke yake ndiye ambaye ndani yake watu wanaweza kupata hazina zote za hekima na ufahamu zilizofichwa katika Kristo. Nawaambia hili ili asiwepo yeyote atakaye wadanganya kwa maneno na hoja zinazoonekana kuwa ni nzuri, lakini ni mbaya. Ingawa niko mbali kimwili, niko pamoja nanyi katika roho. Ninafurahi kuona jinsi mnavyofanya kazi vizuri pamoja na jinsi imani yenu ilivyo thabiti katika Kristo. Mlimpokea Kristo Yesu kama Bwana, hivyo mwendelee kumfuata yeye. Na mizizi yenu ikue hata ndani ya Kristo, na maisha yenu yajengwe juu yake. Kama mlivyofundishwa imani ya kweli mwendelee kuwa imara katika ufahamu wenu katika hilo. Na msiache kumshukuru Mungu. Angalieni msichukuliwe mateka na mafundisho ya uongo kutoka kwa watu wasio na chochote cha maana kusema, bali kuwadanganya tu. Mafundisho yao hayatoki kwa Kristo bali ni desturi za kibinadamu tu na zinatoka katika nguvu za uovu zinazotawala maisha ya watu. Nasema hili kwa sababu Mungu mwenyewe kama alivyo, ukamilifu wa uungu wake unaishi ndani ya Kristo. Hii ni hata wakati wa maisha yake hapa duniani. Na kwa sababu ninyi ni wa Kristo basi mmekamilika, na mna kila kitu mnachohitaji. Kristo ni mtawala juu ya kila nguvu na mamlaka zingine zote. Mlitahiriwa katika Kristo kwa namna tofauti, si kwa mikono ya kibinadamu. Hii ni kusema ya kwamba, mlishiriki katika kifo cha Kristo, ambacho kilikuwa aina ya tohara kwa namna ya kuuvua mwili wake wa kibinadamu. Na mlipobatizwa, mlizikwa na kufufuka pamoja naye kutokana na imani yenu kwa nguvu za Mungu aliyemfufua Kristo kutoka katika kifo. Mlikuwa wafu kiroho kwa sababu ya dhambi zenu na kwa sababu hamkuwa sehemu ya watu wa Mungu. Lakini Mungu amewapa ninyi uhai mpya pamoja na Kristo na amewasamehe dhambi zenu zote. Kwa sababu tulizivunja sheria za Mungu, tunalo deni. Kumbukumbu ya deni hilo imeorodhesha amri zote tulizoshindwa kuzifuata. Lakini Mungu ametusamehe deni hilo. Ameiondoa kumbukumbu yake na kuipigilia msalabani. Pale msalabani, aliwanyang'anya watawala wa ulimwengu wa roho nguvu na mamlaka. Aliwashinda pale. Na akawafukuza kama wafungwa ili ulimwengu wote uone. Hivyo msimruhusu mtu yeyote awahukumu katika masuala yanayohusu kula au kunywa au kwa kutofuata desturi za Kiyahudi (kusherehekea siku takatifu, sikukuu za Mwandamo wa Mwezi, au siku za Sabato). Zamani mambo hayo yalikuwa kama kivuli cha yale yaliyotarajiwa kuja. Lakini mambo mapya yaliyotarajiwa kuja yanapatikana katika Kristo. Watu wengine hufurahia kutenda mambo yanayowafanya wajisikie kuwa ni wanyenyekevu na kisha kushirikiana na malaika katika ibada. Nao wanazungumza juu ya kuyaona mambo hayo katika maono. Msiwasikilize wanapowaambia kuwa mnakosea kwa sababu hamfanyi mambo haya. Ni ujinga kwao kujisikia fahari kwa kufanya hivyo, kwa sababu mambo hayo yote yanatokana na namna mwanadamu anavyofikiri. Hawajafungamanishwa na kichwa; Kristo ndiye kichwa, na mwili wote humtegemea Yeye. Kwa sababu ya Kristo viungo vyote vya mwili vinatunzana na kusaidiana kila kimoja na kingine. Hivyo mwili hupata nguvu zaidi na kufungamana pamoja kadri Mungu anavyouwezesha kukua. Mlikufa pamoja na Kristo na kuwekwa huru kutoka katika nguvu zinazotawala dunia. Hivyo kwa nini mnaishi kama watu ambao bado mngali wa ulimwengu? Nina maana kuwa, kwa nini mnafuata sheria hizi: “Usile hiki”, “Usionje kile”, “Usiguse kile”? Sheria hizi zinazungumzia vitu vya kidunia, vitu vinavyotokomea baada ya kutumiwa. Ni amri na mafundisho ya kibinadamu tu. Sheria hizi zinaweza kuonekana za busara kama sehemu ya dini zilizoundwa na watu ambamo watu huiadhibu miili yao na kutenda mambo yanayowafanya wajisikie wanyenyekevu. Lakini sheria hizi haziwasaidii watu kuthibiti tamaa zao za udhaifu wa kibinadamu. Mlifufuka pamoja na Kristo kutoka kwa wafu. Hivyo ishini maisha mapya, mkiyatazamia yaliyo mbinguni, ambako Kristo ameketi mkono wa kulia wa Mungu. Msiyafikirie yaliyo hapa duniani bali yaliyo mbinguni. Utu wenu wa kwanza umekufa, na utu wenu mpya umetunzwa na Kristo katika Mungu. Kristo ndiye utu wenu mpya sasa, na atakaporudi mtashiriki katika utukufu wake. Kwa hiyo kiueni chochote kilicho cha kidunia kilichomo ndani yenu: uasherati, matendo machafu, mawazo na tamaa mbaya. Msijitakie na kujikusanyia vitu vingi, kwani ni sawa na kuabudu mungu wa uongo. Mungu ataionyesha hasira yake kwa wale wasiomtii, kwa sababu ya maovu wanayotenda. Ninyi pia mlifanya maovu haya huko nyuma, mlipoishi kama wao. Lakini sasa, jitengeni mbali na mambo haya katika maisha yenu: hasira, ukorofi, chuki, na mazungumzo yenye matusi. Msiambiane uongo ninyi kwa ninyi. Ninyi mmeyavua mavazi ya kale; utu wa kale mliokuwa nao na matendo mabaya mliyotenda hapo awali. Na sasa mmevaa utu mpya unaofanywa upya kila siku hata kuufikia ufahamu kamili wa Kristo. Mfano wenu wa maisha mapya ni Kristo, aliye mfano na sura ya Mungu aliyewaumba ninyi. Katika utu huu mpya haijalishi ikiwa wewe ni Myunani au Myahudi, umetahiriwa au hujatahiriwa. Haijalishi pia ikiwa unazungumza lugha tofauti au hata kama wewe ni mtu asiyestaarabika, ikiwa ni mtumwa ama mtu huru. Kristo ndiye wa muhimu zaidi, naye yumo ndani yenu ninyi nyote. Mungu amewachagua na kuwafanya ninyi kuwa watu wake walio watakatifu. Anawapenda. Hivyo, jivikeni matendo haya na muwe na huruma: wema, wanyenyekevu, wapole na wenye subira. Msikasirikiane, bali msameheane. Mtu yeyote akikukosea, msamehe. Wasameheni wengine kwa sababu Bwana amewasamehe ninyi. Pamoja na haya yote, vaeni upendo. Upendo ndicho kitu kinachounganisha kila kitu katika umoja mkamilifu. Amani inayotoka kwa Kristo itawale fahamu zenu. Mliitwa kwa ajili ya amani ili muwe pamoja katika mwili mmoja. Mwe na shukrani daima. Na mafundisho ya Kristo yakae kwa wingi ndani yenu. Mfundishane na mshauriane ninyi kwa ninyi kwa hekima yote, mkiimba zaburi, nyimbo za sifa na nyimbo zinaowezeshwa na roho na kumshukuru Mungu katika mioyo yenu. Kila mnachosema na kutenda, mkifanye kwa ajili ya Yesu Kristo Bwana wenu huku mkimshukuru Mungu Baba kupitia Yesu Kristo. Wake, muwe radhi kuwatumikia waume zetu. Ni jambo sahihi kufanya katika kumfuata Bwana. Waume wapendeni wake zenu na msiwe na hasira nao. Watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote. Hili humfurahisha Bwana. Wababa, msiwakorofishe watoto wenu, mkiwa wagumu kupendezwa nao; wanaweza kukata tamaa. Enyi watumwa, watiini mabwana zenu katika mambo yote. Mwe watii kila wakati, hata kama wao hawawezi kuwaona. Msijifanye kazi kwa bidii ili wawatendee mema. Mnapaswa kuwatumikia mabwana zenu kwa moyo kwa sababu mna hofu ya Bwana. Kila kazi mnayoifanya, ifanyeni kwa bidii. Fanyeni kama mnamfanyia Bwana wenu wa mbinguni, na si kama mnamfanyia bwana wa dunia hii. Mnajua kwamba mtapokea kutoka kwa Bwana ujira aliowaahidi watu wake. Ndiyo, mnamtumikia Kristo aliye Bwana wenu halisi. Kumbukeni kuwa Mungu hana upendeleo; kila afanyaye uovu ataadhibiwa kwa sababu ya uovu wake. Enyi mabwana, wapeni kilicho chema na chenye haki watumwa wenu. Kumbukeni kuwa Mkuu wenu yuko mbinguni. Msiache kuomba kamwe. Iweni tayari kwa lolote kwa kuomba na kushukuru. Mtuombee na sisi pia, ili Mungu atupe fursa za kuwaeleza watu ujumbe wake. Nimefungwa kwa sababu ya hili. Lakini ombeni ili tuendelee kuwaeleza watu siri ya kweli ambayo Mungu ameiweka wazi kuhusu Kristo. Niombeeni ili niseme yanayonipasa kusema, ili niweze kuiweka wazi kweli hii kwa kila mtu. Iweni na hekima kwa namna mnavyochukuliana pamoja na wale wasioamini. Tumieni muda wenu vizuri kadri mwezavyo. Kila mnapozungumza pamoja na walio nje ya kundi lenu, muwe wema na wenye hekima. Ndipo mtaweza kumjibu kila mtu ipasavyo. Tikiko ni ndugu yangu mpendwa katika Kristo. Yeye ni msaidizi mwaminifu na anamtumikia Bwana pamoja nami. Atawaambia kila kitu kuhusu mimi. Hii ndiyo sababu ninamtuma, ninataka mfahamu hali yetu, na ninamtuma awatie moyo ninyi. Ninamtuma yeye pamoja na Onesimo, ndugu mpendwa na mwaminifu kutoka kwenye kundi lenu. Watawaeleza kila kitu kilichotokea hapa. Aristarko, aliyefungwa pamoja nami humu gerezani anawasalimu. Marko, binamu yake Barnaba anawasalimu pia. (Nimekwisha kuwaambia kuhusu Marko. Ikiwa atakuja, mpokeeni.) Pia pokeeni salamu toka kwa Yesu, aitwaye pia Yusto. Hawa ni Wayahudi waamini pekee wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Wamekuwa faraja kubwa sana kwangu. Epafra, mtumishi mwingine wa Yesu Kristo, kutoka kwenu anawasalimu. Yeye anahangaika kwa ajili yenu kwa kuwaombea mara kwa mara, ili mkue kiroho na kupokea kila kitu ambacho Mungu anataka kwa ajili yangu. Ninafahamu kwamba amefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu ninyi na kwa ajili ya watu wa Laodikia na Hierapoli. Pokeeni pia salamu kutoka kwa Dema na kutoka kwa rafiki yetu mpendwa Luka ambaye ni tabibu. Wasalimuni kaka na dada zetu walioko Laodikia. Msalimuni pia Nimfa na kanisa lililo katika nyumba yake. Baada ya kusoma barua hii, ipelekeni katika kanisa la Laodikia, ili isomwe huko pia. Ninyi nanyi msome barua niliyowaandikia wao. Mwambieni Arkipo hivi, “Hakikisha unaifanya kazi aliyokupa Bwana.” Hii ni salamu yangu ambayo nimeiandika kwa mkono wangu mwenyewe: PAULO. Msiache kunikumbuka nikiwa hapa gerezani. Ninawaombea neema ya Mungu iwe pamoja nanyi nyote. Salamu toka kwa Paulo, Sila, na Timotheo. Kwa kanisa lililoko Thesalonike lililo milki ya Mungu baba na Bwana Yesu Kristo. Neema na amani ziwe zenu. Kila mara tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu nyote na kuwataja katika maombi yetu. Kila tunapomwomba Mungu baba yetu, tunawakumbuka kwa yote mliyofanya kwa sababu ya imani yenu. Na tunawakumbuka kwa kazi mliyofanya kwa sababu ya upendo wenu. Na tunakumbuka jinsi mlivyo imara kwa sababu ya tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo. Ndugu zetu, Mungu anawapenda. Nasi twajua yakuwa amewachagua muwe watu wake. Tulipowaletea Habari Njema kwenu, tulikuja na yaliyo zaidi ya maneno. Tuliwaletea ile Habari Njema yenye uweza, pamoja na Roho Mtakatifu, na tulikuwa na uhakika kamili hiyo ilikuwa ni Kweli halisi. Pia mnafahamu tulivyo enenda tulipo kuwa pamoja nanyi. Tuliishi hivyo ili kuwasaidia ninyi. Nanyi mkauiga mfano wetu na mfano wa Bwana. Mliteseka sana, lakini bado mliyakubali mafundisho na furaha inayotokana na Roho Mtakatifu. Mlifanyika mfano wa kuigwa na waaminio wote wa Makedonia na Akaya. Mafundisho ya Bwana yameenea toka Makedonia mpaka Akaya na nje ya mipaka yake. Kwa kweli, imani yenu katika Mungu imejulikana kila mahali, hivyo hatuna haja ya kumwambia mtu yeyote kwa habari hii. Watu kila mahali wanasimulia habari ya namna mlivyotupokea vizuri tulipo kuwa pamoja nanyi. Wanasimulia namna mlivyoacha kuiabudu miungu ya uongo na kubadilika na kuanza kumwabudu Mungu aliye hai na wa kweli. Na mkaanza kumngoja mwana wa Mungu aje kutoka mbinguni, Mwana ambaye Baba alimfufua kutoka kwa wafu. Yeye ni Yesu, anayetuokoa kutoka katika hukumu yenye hasira ya Mungu inayokuja. Ndugu zangu, mnafahamu kuwa safari yetu kuja kwenu ilikuwa yenye nguvu. Lakini kabla ya kuja kwenu, watu wa Filipi walitutenda vibaya kwa kututukana matusi mengi na kutusababishia mateso. Mnafahamu yote kuhusu hilo. Na kisha tulipokuja kwenu, watu wengi huko walitupinga. Tuliwaeleza ninyi Habari Njema za Mungu lakini ni kwa sababu Mungu alitupa ujasiri tulio hitaji. Hatukuwa na kitu cha kupata faida kwa kuwaomba ninyi muiamini Habari Njema. Hatukuwa tunataka kuwafanya wajinga wala kuwadanganya. Hapana, tulifanya hivyo kwa sababu Mungu ndiye aliyetuagiza kazi hii. Na hii ilikuwa baada ya yeye kutupima na kuona ya kuwa tunaweza kuaminiwa kuifanya. Hivyo tunapoongea, tunajaribu tu kumpendeza Mungu, na sio wanadamu. Yeye tu ndiye awezaye kuona kilichomo ndani yetu. Mnafahamu kuwa hatukujaribu kuwarubuni kwa kusema mambo mazuri juu yenu. Hatukuwa tunatafuta jinsi ya kuzichukua pesa zenu. Hatukutumia maneno ama matendo kuficha tamaa yetu. Mungu anajua ya kuwa huu ni ukweli. Hatukuwa tukitafuta sifa toka kwa watu ama kutoka kwenu au kwa mtu yeyote. Tulipokuwa pamoja nanyi, kama mitume wa Kristo tulikuwa na uwezo wa kutumia mamlaka yetu kuleta madai ya nguvu kwenu. Lakini tulikuwa wapole kwenu. Tulikuwa kama vile mkunga anavyowahudumia watoto wake wadogo. Ilikuwa ni upendo wetu mkuu sana kwenu uliotufanya tuwashirikishe Habari Njema za Mungu. Zaidi ya hayo yote tulifurahi kuwashirikisha ninyi nafsi zetu wenyewe. Hiyo inadhihirisha ni kwa kiwango gani tuliwapenda. Ndugu zangu, ninajua kuwa mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi kwa bidii. Tulifanya kazi usiku na mchana ili tujitegemee, pasipo kumwelemea mtu yeyote wakati tukifanya kazi ya kuhubiri Habari Njema za Mungu. Tulipokuwa pamoja nanyi enyi mnaoamimi, tulikuwa safi, wa kweli, na wasio na kosa lolote kwa namna tulivyoishi maisha matakatifu. Mnafahamu, kama vile Mungu anavyotenda, kuwa jambo hili ni la kweli. Mnafahamu jinsi tulivyo mtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea wanaye. Tuliwatia moyo, tuliwafariji, na tuliwaambia kuishi maisha mema kwa Mungu. Yeye anawaita muwe sehemu ya maisha mema mbele za Mungu. Pia, tunamshukuru Mungu pasipo kuacha kwa sababu ya namna mlivyoupokea ujumbe wake. Ingawa tuliuleta kwenu, mliupokea si kama ujumbe unaotoka kwa wanadamu, bali kama ujumbe wa Mungu. Kweli hakika ni ujumbe kutoka kwa Mungu, unaofanya kazi kwenu ninyi mnao uamini. Kaka na dada zangu katika Bwana, mmeufuata mfano wa makanisa ya Mungu yaliyoko Uyahudi yaliyo mali ya Kristo Yesu. Nina maana ya kuwa ninyi mlitendewa vibaya na watu wa kwenu, namna ile ile walioamini wa Kiyahudi walivyotendewa vibaya na Wayahudi wenzao. Wayahudi wengine pia walimuua Bwana Yesu na manabii. Na walitulazimisha sisi kuondoka katika mji lenu. Hawampendezi Mungu, na wako kinyume na watu wengine wote. Na wanajaribu kutuzuia tusizungumze na wasio Wayahudi. Wanapofanya hivi wanawazuia watu wasio Wayahudi kuokoka. Na hivyo wanaendelea kuziongeza dhambi zao hata kujaza kipimo. Sasa wakati umefika kwa wao kuadhibiwa na hasira ya Mungu. Kaka na dada zangu, tulikuwa kama yatima, tulitengwa nanyi kwa muda. Lakini hata kama hatukuwa pamoja nanyi, mawazo yetu yalikuwa bado yangali nanyi. Tulitamani sana kuwaona, na tulijitahidi sana kulitimiza hilo. Ndiyo, tulitamani kuja kwenu. Mimi, Paulo, nilijaribu zaidi ya mara moja kuja kwenu, lakini Shetani alituzuia. Ninyi ni tumaini letu, furaha yetu, na taji yetu tutakayojivunia wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu. Mnatuletea heshima na furaha. Nisingeweza kuja kwenu, ila ilikuwa vigumu kuendelea kusubiri zaidi. Hivyo tuliamua kumtuma Timotheo kwenu na tukabaki Athene peke yetu. Timotheo ni ndugu yetu. Ni mtenda kazi pamoja nasi kwa ajili ya Mungu katika kuwahubiri watu Habari Njema kuhusu Kristo. Nilimtuma Timotheo kuwaimarisha na kuwafariji katika imani yenu. *** Tulimtuma ili asiwepo kati yenu atakayebugudhiwa na mateso tuliyo nayo sasa. Ninyi wenyewe mnatambua kuwa ni lazima tupatwe na mateso haya. Hata pale tulipokuwa pamoja nanyi, tuliendelea kuwaeleza mapema ya kuwa sote tutapata matatizo. Na mnafahamu kuwa ilitokea kama tulivyowaambia. Hii ndiyo sababu nilimtuma Timotheo kwenu, ili nipate kujua juu ya uaminifu wenu. Nilimtuma kwenu nilipokuwa siwezi kuendelea kusubiri zaidi. Nilihofu kuwa Shetani angeweza kuwashinda kwa majaribu yake. Kisha kazi yetu iliyokuwa ngumu ingepotea bure. Bali sasa Timotheo amerudi kutoka kwenu na kutueleza juu ya uaminifu wenu na upendo wenu. Ametueleza kuwa mmeendelea kuwa na kumbukumbu njema juu yetu kama mfano kwenu. Na amesema kuwa mnatamani sana kutuona tena. Hivyo ndivyo ilivyo kwetu pia tunatamani sana kuwaona ninyi. Kwa hiyo, ndugu zangu, tunatiwa moyo sana kwa ajili ya uaminifu wenu. Tunapata mateso na masumbufu mengi, lakini bado tunatiwa moyo nanyi. Kwa kuwa sasa tuna maisha mapya tunapata utimilifu ikiwa imani yenu katika Bwana inaendelea kuwa imara. Tuna furaha tele mbele za Mungu wetu kwa ajili yenu! Lakini hatuwezi kumshukuru Mungu inavyopasa kwa furaha ile yote tuliyo nayo. Usiku na mchana tuliendelea kuomba kwa mioyo yetu yote kwamba tuweze kuja huko na tuwaone tena. Tunataka kuwapa kila mnachohitaji ili imani yenu iwe timilifu. Tunaomba kwamba Mungu wetu aliye Baba yetu, na Bwana Yesu wataiongoza njia yetu kuja kwenu. Tunaomba kuwa Bwana ataufanya upendo wenu uendelee kukua. Tunaomba kuwa atawapa kupendana zaidi na zaidi miongoni mwenu na kwa watu wote. Tunaomba kuwa mtampenda kila mmoja kwa namna ile ile ambayo sisi tuliwapenda ninyi. Hii itaongeza hamu yenu ya kutenda yaliyo haki, na mtakuwa watakatifu msio na kosa mbele za Mungu wetu na baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapo kuja na watakatifu wake wote. Kaka na dada zangu sasa nina mambo mengine ya kuwaambia. Tuliwafundisha namna ya kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Nanyi mnaishi hivyo. Na sasa tunawaomba na kuwatia moyo katika Bwana Yesu kuishi zaidi na zaidi katika njia hiyo. Mnafahamu yote tuliyowaamuru kufanya kwa mamlaka ya Bwana Yesu Kristo. Mungu anawataka muwe watakatifu. Anawataka mkae mbali na dhambi za zinaa. Mungu anawataka kila mmoja wenu ajifunze kuuthibiti mwili wake mwenyewe. Tumieni miili yenu kwa namna iliyo takatifu na yenye heshima. Msiruhusu tamaa za mwili kuwatawala kama watu wasiomjua Mungu. Msimtendee vibaya ndugu aliye mwamini wala kuwadanganya katika hili. Bwana atawahukumu watendao hivyo. Tumekwisha kuwaambia juu ya hili na kuwaonya. Mungu alituita kuwa watakatifu na safi. Hivyo kila anayekataa kuyatii mafundisho haya anakataa kumtii Mungu, siyo wanadamu. Na Mungu ndiye anayewapa ninyi Roho Mtakatifu. Hatuna haja ya kuwaandikia juu ya kuwa na upendo kwa katika Kristo. Mungu amekwisha kuwafundisha kupendana ninyi kwa ninyi. Ukweli ni kuwa, mnawapenda wanaoamini wote walioko Makedonia. Tunawatia moyo sasa, kuuonyesha upendo wenu zaidi na zaidi. Fanyeni kila mnaloweza kuishi maisha ya amani. Mjishugulishe na mambo yenu wenyewe, na mfanye kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaambia mwanzo. Mkifanya mambo haya, ndipo wale wasioamini wataheshimu namna mnavyoishi. Na hamtawategemea wengine. Kaka na dada, tunawataka mfahamu habari za wale waliokufa. Hatupendi muwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. Tunaamini kuwa Yesu alikufa, ila tunaamini pia kuwa alifufuka. Hivyo tunaamini kuwa Mungu atawaleta katika uzima kupitia Yesu kila aliyekufa na kukusanywa pamoja naye. Tunalowaambia sasa ni ujumbe wake Bwana. Sisi ambao bado tu hai Bwana ajapo tena tutaungana nae, lakini hatutawatangulia wale waliokwisha kufa. Bwana mwenyewe atakuja kutoka mbinguni pamoja na sauti kuu yenye agizo, na sauti kubwa kutoka kwa malaika mkuu, na ishara ya Mungu ya mlio wa tarumbeta. Na watu waliokufa walio wake Kristo watafufuliwa kwanza. Baada ya hayo, sisi ambao bado tungali hai mpaka wakati huo tutakusanywa pamoja na wale waliokwisha kufa. Tutachukuliwa juu mawinguni na kukutana na Bwana angani. Na tutakuwa na Bwana milele. Hivyo tianeni moyo ninyi kwa ninyi kwa maneno haya. Na sasa ndugu zangu, hatuna haja ya kuwaandikia juu ya nyakati na tarehe. Ninyi mnafahamu vizuri kuwa siku ambayo Bwana atakuja itakuwa ya kushitukiza, kama mwizi anavyokuja usiku. Watu watasema, “tuna amani na tuko salama.” Wakati huo ndipo uharibifu utakapowajia haraka, kama maumivu anayoyapata mwanamke anapojifungua. Na watu hao hawataweza kukwepa. Lakini ninyi ndugu zangu, hamuishi katika giza. Na hivyo ile siku haitawashangaza kama mwivi. Nyote ni watu wa nuru. Ni watu wa mchana. Hatuko katika usiku wala giza. Hivyo tusiwe kama watu wengine. Tusiwe wasinziao. Tuwe macho na wenye kiasi. Watu walalao, hulala usiku. Watu wanywao kupita kiasi, hunywa usiku. Bali sisi ni watu wa mchana, hivyo tujitawale wenyewe. Tuvae imani na upendo vitulinde. Na tumaini la wokovu liwe kwetu kama kofia ya vita. Mungu hakutuchagua tuangamie katika hasira yake. Mungu alituchagua tuwe na wokovu katika Bwana wetu Yesu Kristo. Yesu alikufa kwa ajili yetu ili tuishi pamoja nae. Haijalishi kama tu hai au wafu atakapokuja. Hivyo farijianeni ninyi kwa ninyi na msaidiane kukua imara katika imani, kama mnavyofanya sasa. Tunawaomba mwatambue wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao, kama wafuasi wa Bwana, wanatumika kama viongozi wenu na kuwafundisha namna ya kuishi. Wapeni heshima ya hali ya juu na upendo kwa sababu ya kazi wanayofanya. Ishini kwa amani kila mmoja na mwenzake. Tunawasihi, kuwaonya wale wanaokataa kuishi kwa kuwajibika. Watieni moyo wanaoogopa. Wasaidieni walio dhaifu. Mvumilieni kila mmoja. Asiwepo anae jaribu kulipiza baya kwa baya. Lakini kila mara mfanye lililo jema kwa kila mmoja wenu na kwa watu wote. Mwe na furaha daima. Msiache kuomba. Shukuruni kwa kila jambo. Hivi ndivyo Mungu anavyotutaka tuishi katika Kristo Yesu. Msiizimishe kazi ya Roho Mtakatifu. Msiuchukulie unabii kama kitu kisicho cha muhimu. Lakini pimeni kila kitu. Lishikeni lililo jema, na mkae mbali na kila aina ya ovu. Tunaomba kwamba Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, atawafanya muwe watakatifu mkiwa wake. Tunaomba kwamba katika roho yote, nafsi yote, na mwili mzima mtahifadhiwa salama pasipo lawama Bwana wetu Yesu Kristo atakapokuja. Yeye awaitae atawatendea haya. Mnaweza kumtumainia. Kaka na dada zangu, tafadhali mtuombee. Wasalimuni ndugu wote kwa salamu maalum ya watu wa Mungu. Ninawaagiza kwa mamlaka ya Bwana kuusoma walaka huu kwa waamini wote huko. Neema ya Bwana wetu Yesu kristo iwe nanyi nyote. Salamu kutoka kwa Paulo, Sila na Timotheo. Kwa kanisa la Thesalonike lililo mali ya Mungu baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo. Neema na amani viwe kwenu kutoka kwa Mungu Baba na Bwana wetu Yesu Kristo. Kaka na dada zetu, tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu. Na hivyo ndivyo tunavyopaswa kufanya, kwani mnatupa sababu ya kushukuru na imani yenu inakua zaidi na zaidi. Pamoja na hilo upendo ambao kila mmoja wenu anao kwa mwenzake nao unakua. Hivyo tunayaeleza makanisa mengine ya Mungu namna tunavyojivuna kuhusu ninyi. Tunawaeleza jinsi mlivyoendelea kwa subira kuwa imara na waaminifu, ingawa mnateswa na kusumbuliwa na matatizo mengi. Huu ni uthibitisho kwamba Mungu ni wa haki katika hukumu zake. Hutaka kuwastahilisha katika ufalme wake. Kuteswa kwenu ni kwa ajili ya ufalme huo. Ni haki kwa Mungu kuwaadhibu wale wanaowaletea matatizo. Atawaletea unafuu wanaoteseka. Atawaletea ninyi nasi unafuu huo atakapokuja Bwana Yesu kutoka mbinguni ili wote wamwone, pamoja na malaika wake wenye nguvu zilizotukuka. Atakuja na moto unaoteketeza kuwaadhibu wasiomjua Mungu na wanaokataa kuitii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu. Wataadhibiwa na maangamizi yasio na mwisho. Hawataruhusiwa kuwa na Bwana lakini watatengwa mbali na nguvu zake za utukufu. Hii itatokea siku ambapo Bwana Yesu atakuja na kupokea heshima miongoni mwa watu wake watakatifu. Na wote wanaomwamini watamstaajabu. Na hii inawajumuisha ninyi kwa sababu mliamini yale tuliyowaambia. Hii ndiyo sababu daima tunawaombea. Tunamwomba Mungu wetu awasaidie kuishi katika njia njema aliyoitaka alipowachagua. Wema mlionao unawafanya mtake kufanya mema. Na imani mliyonayo inafanya mfanye kazi. Tunaomba kwamba kupitia nguvu zake Mungu atayakamilisha yote mema mliyokusudia kufanya pamoja na kazi zote zinazotokana na imani yenu. Kisha jina la Bwana wetu Yesu litaheshimiwa kwa sababu yenu, nanyi mtaheshimiwa kwa sababu yake, na mtaheshimiwa kwa sababu yake. Hii inaweza kutokea tu kwa neema ya Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo. Kaka na dada, tuna jambo la kuwaambia juu ya kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunataka kuzungumza nanyi juu ya wakati huo tutakapokusanyika pamoja naye. Msikubali kufadhaishwa na kutiwa kuhofu ikiwa mtasikia kwamba siku ya Bwana tayari imekwishawadia. Wengine wanaweza kusema kwamba wazo hili limetoka kwetu katika jambo alilotuambia Roho, au tulilosema, au katika barua tuliyoiandika. Msidanganywe na chochote wanachoweza kusema kuhusu kuja kwa Bwana. Siku hiyo ya Bwana haitakuja mpaka itanguliwe na kukengeuka kwa wanadamu na kumwacha Mungu. Na siku hiyo haitakuja mpaka ajitokeze kwanza Mtu wa Uovu, yule ambaye ana uhakika kuwa ataangamizwa. Huyo atasimama kinyume na kujiweka mwenyewe juu ya kila kitu ambacho watu wanaabudu au kudhani kuwa kinafaa kuabudiwa. Ataenda na kuingia ndani ya Hekalu na kukikalia kiti cha enzi, akidai kuwa yeye ni Mungu. Niliwaambia zaidi ya mara moja nilipokuwa huko kwamba mambo yote haya yangetokea. Je, mnakumbuka? Na mnafahamu kinachomzuia Mtu wa Uovu. Huyo hataruhusiwa kuonekana mpaka wakati sahihi utakapofika. Tayari nguvu ya uovu inatenda kazi ulimwenguni sasa. Lakini yupo mmoja anayeizuia nguvu hiyo. Na ataendelea kuizuia mpaka atakapoondolewa. Kisha huyo Mtu wa Uovu atatokea. Lakini Bwana Yesu atamuua kwa pumzi inayotoka katika kinywa chake. Bwana atakuja katika namna ambayo kila mtu atamwona, na huo utakuwa mwisho wa Mtu wa Uovu. Kuja kwa Mtu wa Uovu itakuwa kazi ya Shetani. Atakuja na nguvu kuu, na atafanya aina zote za miujiza ya uongo, ishara, na maajabu. Mtu wa Uovu atatumia kila aina ya uovu kuwatia ujinga wote walio njiani kuelekea kuangamia. Wamepotea kwa sababu walikataa kuupenda ujumbe wenye ukweli kuhusu Yesu na kuokolewa. Hivyo Mungu atawaacha wadanganyike hata kuamini uongo. Wote watahukumiwa kwa sababu hawakuamini ujumbe wa kweli na kwa kuwa walifurahia kufanya maovu. Ndugu zangu, ninyi ni watu mnaopendwa na Bwana. Na imetupasa tumshukuru Mungu daima kwa sababu yenu. Hayo ndiyo tunayotakiwa kuyatenda, kwa sababu Mungu aliwaita kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuokolewa. Mmeokolewa na Roho aliyewafanya muwe watu wa Mungu walio watakatifu kupitia kuiamini kweli. Mungu aliwaita ninyi mpate wokovu. Aliwaita kwa kutumia Habari Njema tuliwahubiri. Mliitwa ili mshiriki katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo simameni imara na kuendelea kuamini mafundisho tuliyowapa tulipokuwa huko na kupitia barua yetu. Tunaomba kwamba Bwana Yesu Kristo na Mungu Baba yetu awafariji na kuwaimairisha katika kila jambo jema mnalotenda na kusema. Mungu alitupenda na kutupa kupitia neema matumaini ya ajabu na faraja isiyo na mwisho. Na sasa, ndugu zangu, mtuombee. Ombeni kwamba mafundisho ya Bwana yaendelee kuenea haraka na kwamba watu watayaheshimu, kama ilivyotokea kwenu. Mtuombee tupate ulinzi kutokana na watu wabaya na waovu. Mnafahamu, siyo wote wanamwamini Bwana. Lakini Bwana ni mwaminifu. Atawapa nguvu na ulinzi dhidi ya Mwovu. Tuna uhakika kwa sababu ya Bwana mnayemtumikia na mtaendelea kuyafanya yale tunayowaamuru. Tunaomba kwamba Bwana atasababisha mjisikie upendo wa Mungu na kukumbuka subira ya ustahimilivu wa Kristo. Kwa mamlaka ya Bwana wetu Yesu Kristo tunawaambia kukaa mbali na mwamini yeyote anayekataa kufanya kazi. Watu kama hao wanaokataa kufanya kazi hawafuati mafundisho tuliyowapa. Ninyi wenyewe mnafahamu kwamba mnatakiwa kuishi kwa kuiga mfano wetu. Hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi wala hatukuishi pasipo utaratibu unaofaa. Hatukupokea chakula kutoka kwa yeyote bila ya kukilipia. Tulifanya kazi ili tusiwe mzigo kwa yeyote. Tulifanya kazi usiku na mchana. Tulikuwa na haki ya kuomba mtusaidie. Lakini tulifanya kazi ili tuwe mfano wa kuigwa nanyi. Tulipokuwa nanyi, tuliwapa kanuni hii: “Yeyote asiyefanya kazi asile.” Tunasikia kwamba watu wengine katika kundi lenu wanakataa kufanya kazi. Hawashughuliki kufanya kazi badala yake wanashughulika kwa kuyafuatilia maisha ya wengine. Maagizo yetu kwao ni kuwakataza kuwasumbua wengine, waanze kufanya kazi na kupata chakula chao wenyewe. Ni kwa mamlaka ya Bwana Yesu Kristo tuwaagize kufanya hivi. Msichoke kabisa kutenda wema. Wakiwapo wengine huko wanaokataa kufanya tunayowaambia katika barua hii, basi mkumbuke wao ni kina nani. Msichangamane nao. Ndipo pengine wanaweza kujisikia aibu. Lakini msiwafanye kama adui. Washaurini waachane na tabia hiyo kama watu wa nyumbani mwake Mungu. Tunaomba kwamba Bwana wa amani awape amani wakati wote na kwa njia yo yote. Bwana atakuwa pamoja nanyi nyote. Hizi ni salamu zangu kwa mwandiko wangu: PAULO. Ninafanya hivi katika barua zangu zote kuonesha zinatoka kwangu. Hivi ndivyo ninavyoandika. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu. Mimi ni mtume kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu atupaye tumaini. Ninakuandikia wewe, Timotheo. Wewe ni kama mwanangu halisi kwa sababu ya imani yetu. Neema, rehema na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu ziwe pamoja nawe. Nilipokwenda Makedonia, nilikuomba ubaki Efeso. Baadhi ya watu huko wanafundisha mambo yasiyo ya kweli, nami ninataka uwaonye waache. Uwaambie wasitumie muda wao kusimulia simulizi zisizo na maana za mambo ya kale na kutengeneza orodha ndefu ya mababu. Mambo hayo husababisha mabishano tu na hayaisaidii katika kuikamilisha kazi ya Mungu tuliyopewa, ambayo ni lazima tuikamilishe kwa imani. Kusudi langu la kukueleza ufanye jambo hili ni kutaka kukuza upendo; aina ya upendo unaooneshwa na wale ambao mawazo yao ni safi; watu ambao hufanya yale wanayojua kuwa ni sahihi na ambao imani yao kwa Mungu ni ya kweli. Lakini wengine wamekosa jambo hili la msingi katika mafundisho yao na wamepoteza mwelekeo. Sasa wanazungumza juu ya mambo yasiyo na msaada kwa mtu yeyote. Wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawafahamu mambo wanayosema, wanasema kwa ujasiri wote juu ya mambo wasiyoyaelewa wenyewe. Tunajua kwamba sheria ni nzuri ikiwa mtu anaitumia kwa usahihi. Pia tunajua kwamba sheria haikutengenezwa kwa ajili ya wale wanaotenda haki. Imetengenezwa kwa ajili ya wale wanayoipinga na kukataa kuifuata. Sheria ipo kwa ajili ya wenye dhambi wanaompinga Mungu na mambo yote yanayompendeza. Ipo kwa ajili ya wale wasio na hamu ya mambo ya kiroho na kwa ajili ya wale wanaowaua baba au mama zao au mtu yeyote yule. Ipo kwa ajili ya watu wanaotenda dhambi ya uasherati, kwa wanaume wanaolala na wanaume wenzao au wavulana, kwa wote wanaoteka watu na kuwauza kama watumwa, kwa wote wanaodanganya au wale wasiosema ukweli wakiwa katika kiapo, na kwa ajili ya wale walio kinyume na mafundisho ya kweli ya Mungu. Mafundisho hayo ni sehemu ya Habari Njema ambayo Mungu wetu wa utukufu alinipa kuhubiri na ndani yake tunauona utukufu wake. Ninamshukuru Kristo Yesu Bwana wetu kwa sababu aliniamini na kunipa kazi hii ya kumtumikia. Yeye hunitia nguvu ya kufanya kazi hii. Hapo zamani nilimtukana Kristo. Nikiwa mtu mwenye majivuno na mkorofi, niliwatesa watu wake. Lakini Mungu alinihurumia kwa sababu sikujua nilichokuwa nafanya. Nilifanya hayo kabla sijaamini. Lakini Bwana wetu alinipa kiwango kikubwa cha neema yake. Na pamoja na neema hiyo imani na upendo ulio katika Kristo Yesu vilifuata. Huu ndiyo usemi wa kweli unaopaswa kukubaliwa pasipo kuuliza maswali; kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, nami ni mbaya zaidi ya wote. Lakini nilipata rehema kwa sababu ili Kristo Yesu aweze kunitumia, mimi mtenda dhambi kuliko wote, ili kuonesha uvumilivu wake usio na kikomo. Alitaka niwe mfano kwa wale ambao wangemwamini na kupata uzima wa milele. Heshima na utukufu kwa mfalme anayetawala milele. Hawezi kuharibiwa wala kuonekana. Heshima na utukufu apewe Mungu wa pekee milele na milele, Amina. Timotheo wewe ni mwanangu mwenyewe kwa sababu ya ushirika wetu wa imani ya kweli. Ninayokuambia kuyatenda yanakubaliana na unabii ambao ulisemwa juu yako hapo zamani. Nataka uukumbuke unabii huo na kupigana vita vizuri vya imani. Endelea kumwamini Mungu na kutenda yale unayojua kuwa ni sahihi. Watu wengine hawajatenda haya, na imani yao sasa imeharibiwa. Himenayo na Iskanda ni mfano wa watu hao. Nimewakabidhi kwa Shetani ili wafundishwe kutosema kinyume cha Mungu. Kwanza kabisa, ninakuagiza uwaombee watu wote. Uwaombee kwa Mungu ili awabariki na kuwapa mahitaji yao. Kisha umshukuru Yeye. Unapaswa kuwaombea watawala na wote wenye mamlaka. Uwaombee viongozi hawa ili tuweze kuishi maisha yenye utulivu na amani, maisha yaliyojaa utukufu kwa Mungu na yanayostahili heshima. Hili ni jambo jema na linampendeza Mungu Mwokozi wetu. Mungu anataka kila mtu aokolewe na aielewe kweli kikamilifu. Kuna Mungu mmoja tu, na kuna mwanadamu mmoja tu anayeweza kuwaleta pamoja wanadamu wote na Mungu wao. Huyo mtu ni Kristo Yesu kama mwanadamu. Alijitoa mwenyewe kulipa deni ili kila mtu awe huru. Huu ni ujumbe ambao Mungu alitupa wakati unofaa. Nami nilichaguliwa kama mtume kuwaambia watu ujumbe huo. Ninasema kweli. Sidanganyi. Nilichaguliwa kuwafundisha wasio Wayahudi na nimefanya kazi hii kwa imani na ukweli. Nataka wanaume walio kila mahali waombe. Ni lazima wawe watu wanaoishi kwa kumpendeza Mungu na wanaonyoosha mikono yao wanapoomba na wawe watu wasio na hasira na wanaopenda mabishano. Na ninawataka wanawake wajipambe kwa namna inayofaa. Mavazi yao yawe yanayofaa na yanayostahili. Hawapaswi kuvutia watu kwa kutengeneza nywele zao kwa mitindo ya ajabu ama kwa kuvaa dhahabu, vito au lulu au nguo za gharama. Lakini wajipambe na kuvutia kwa matendo mema wanayofanya. Hayo ndiyo yanayofaa zaidi kwa wanawake wanaosema kuwa wamejitoa kwa ajili ya Mungu. Mwanamke anapaswa kujifunza akisikiliza kwa utulivu huku akiwa radhi kutii kwa moyo wake wote. Simruhusu mwanamke kumfundisha mwanaume au kumwelekeza jambo la kufanya. Bali lazima asikilize kwa utulivu, kwa sababu Adamu aliumbwa kwanza na Hawa akaumbwa baadaye. Na Adamu hakudanganywa. Bali mwanamke ndiye aliyedanganywa naye akatenda dhambi. Lakini wanawake wataokolewa kwa jukumu lao la kuzaa watoto. Wakiendelea kuishi katika imani, upendo, utakatifu na tabia njema. Usemi huu ni wa kweli kwamba yeyote mwenye nia ya kuhudumu kama mzee, anatamani kazi njema. Mzee lazima awe mtu mwema asiyelaumiwa na mtu yeyote. Anapaswa kuwa mwaminifu kwa mke wake. Anapaswa kuwa na kiasi, mwenye busara na mwenye mwenendo mzuri katika maisha, anayeheshimiwa na watu wengine, aliye tayari kuwasaidia watu kwa kuwakaribisha katika nyumba yake. Ni lazima awe mwalimu mzuri. Askofu asizoee kunywa mvinyo wala kuwa mgomvi. Bali awe mpole na mtu wa amani, na asiyependa fedha. Ni lazima awe kiongozi mzuri kwa familia yake mwenyewe. Hii ina maana kwamba watoto wake wanamtii kwa heshima zote. Ikiwa mtu hawezi kuiongoza familia yake mwenyewe, hawezi kulitunza Kanisa la Mungu. Ni lazima askofu asiwe yule aliyeamini hivi karibuni. Hii inaweza kumfanya awe na kiburi. Kisha anaweza akahukumiwa kwa kiburi chake kama vile Shetani alivyopanga. Pia, ni lazima askofu aheshimiwe na watu walio nje ya Kanisa. Kwa namna hiyo hataweza kukosolewa na kuabishwa na wengine na kunasa kwenye mtego wa Shetani. Kwa njia hiyo hiyo, watu wanaoteuliwa kuwa mashemasi inawapasa kuwa wale wanaostahili kuheshimiwa. Wasiwe watu wanaosema mambo wasiokuwa nayo moyoni au wanaotumia muda wao mwingi katika ulevi. Wasiwe watu wanaowaibia fedha watu wengine kwa udanganyifu. Ni lazima waifuate imani ya kweli ambayo Mungu ameiweka wazi kwetu na sikuzote wawe watu wanaotenda mambo yaliyo sahihi. Hao unapaswa kuwapima kwanza. Kisha, ukigundua kuwa hawawezi kushitakiwa jambo lolote baya walilotenda, basi wanaweza kuwa mashemasi. Kwa njia hiyo hiyo wanawake wanaoteuliwa kuwa mashemasi wanapaswa kuwa wale wanaoastahili kuheshimiwa. Wasiwe wanawake wanaosema mambo mabaya juu ya watu wengine. Ni lazima wawe na kiasi. Ni lazima wawe wanawake wanaoweza kuaminiwa kwa kila jambo. Wanaume walio mashemasi lazima wawe waaminifu katika ndoa. Ni lazima wawe viongozi wema wa watoto na familia zao binafsi. Mashemasi wanaofanya kazi yao vyema wanajitengenezea nafasi nzuri ya kuheshimiwa. Nao kwa kiasi kikubwa sana wanajihakikishia imani yao katika Kristo Yesu. Ninatarajia kuja kwenu hivi karibuni. Lakini ninakuandikia maneno haya sasa, ili kwamba, hata kama sitakuja mapema, utafahamu jinsi ambavyo watu wanapaswa kuishi katika familia ya Mungu. Familia hiyo ni kanisa la Mungu aliye hai. Na Kanisa la Mungu ni msaada na msingi wa ukweli. Ndiyo, Mungu ametuonesha siri ya maisha yanayompa heshima na kumpendeza Yeye. Siri hii ya ajabu ni ukweli ambao wote tunakubaliana nao: Kristo alijulikana kwetu katika umbile la kibinadamu; alioneshwa na Roho kuwa kama alivyojitambulisha; alionwa na malaika. Ujumbe kuhusu Yeye ulitangazwa kwa mataifa; watu ulimwenguni walimwamini; alichukuliwa juu mbinguni katika utukufu. Roho anasema wazi wazi kwamba katika siku za mwisho wengine watajitenga na imani. Watazitii roho zinazodanganya, na kufuata mafundisho ya mashetani. Mafundisho hayo yanafundishwa na watu wanaodanganya na kuwafanyia hila wengine. Watu hawa waovu hawapambanui kati ya mema na maovu. Ni kana kwamba dhamiri zao zimeharibiwa kwa chuma cha moto. Wanasema ni vibaya kuoa. Na wanasema kwamba kuna baadhi ya vyakula ambavyo watu lazima wasile. Lakini Mungu aliumba vyakula hivi, na wale wanaoamini na kuelewa ukweli wanaweza kuvila kwa shukrani. Kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, hakuna chakula kitakachokataliwa kama kikikubaliwa kwa shukrani. Kila kitu alichokiumba kiliumbwa kitakatifu kwa namna alivyosema na kwa maombi. Waambie haya kaka na dada huko. Hii itakuonesha wewe kuwa ni mtumishi mwema wa Kristo Yesu. Utaonyesha kwamba umefundishwa maneno ya imani na mafundisho mazuri uliyoyafuata. Usitumie muda wowote katika masimulizi ya kipuuzi ambayo hayakubaliani na ukweli wa Mungu. Badala yake jizoeshe mwenyewe kuishi maisha ya kumheshimu na kumpendeza Mungu. Kufanya mazoezi ya mwili wako kuna manufaa kidogo kwako. Lakini kujaribu kumpendeza Mungu kwa njia zote kunakufaa zaidi. Kunakuletea baraka katika maisha haya na maisha ya baadaye pia. Huu ni usemi wa kweli ambao unaweza kukukubaliwa bila kuuliza swali: Tunayo matumaini kwa Mungu aliye hai, Mwokozi wa watu wote. Ambaye hasa, ni Mwokozi wa wale wote wanaomuamini. Na hii ndiyo sababu tunafanya kazi na kupambana. Amuru na kufundisha mambo haya. Wewe ni kijana, lakini usiruhusu yeyote kukufanya wewe kama si mtu muhimu. Uwe mfano kuonesha waamini namna wanavyoweza kuishi. Waoneshe kwa namna unavyosema, unavyoishi, unavyopenda, unavyo amini, na namna ya maisha yako safi. Endelea kusoma Maandiko kwa watu, watie moyo, na uwafundishe. Fanya hivyo mpaka nitakapo kuja. Kumbuka kutumia kipawa ulichonacho, ambacho ulipewa kupitia unabii wakati kundi la wazee lilipo kuweka mikono juu yako. Endelea kufanya haya, na jitoe maisha yako kutenda hayo. Kisha kila mtu anaweza kuona namna ilivyo vema unavyotenda. Uwe mwangalifu katika maisha na mafundisho yako. Endelea kuishi na kufundisha kwa usahihi. Kisha, utajiokoa mwenyewe na wale wanaosikiliza mafundisho yako. Usiseme kwa hasira kwa mtu mzima. Lakini sema naye kama baba yako. Watunze vijana kama kaka zako. Watendee wanawake wazee kama mama zako. Na watendee wanawake vijana kwa heshima zote kama vile ni dada zako. Watunze wajane ambao hasa wanahitaji msaada. Lakini mjane akiwa na watoto au wajukuu, jambo la kwanza ambalo wanahitaji kujifunza ni hili: kutimiza wajibu waliyonao kwa wanafamilia wao. Kwa kuwapa heshima na kuwahudumia, watakuwa wanawalipa fadhila wazazi wao na pia mababu na nyanya zao. Na haya ndiyo mambo yanaompendeza Mungu. Mjane ambaye hakika anahitaji msaada ni yule ambaye ameachwa pekee yake. Anamuamini Mungu kumtunza katika mahitaji yake. Anayemuomba msaada Mungu wakati wote. Lakini mjane anayetumia maisha yake kujipenda ni hakika amekufa angali hai. Wambie waumini huko kutunza familia zao wenyewe ili kwamba asiwepo yeyote atakayesema wanafanya vibaya. Kila mtu atunze watu wa kwao, muhimu sana watunze familia zao. Kama hawatendi hayo watakuwa hawakubaliani na tunayoamini. Watakuwa wabaya kuliko hata asiyeamini. Ili kuongezwa kwenye orodha ya wajane, mwanamke ni lazima awe na umri wa miaka 60 au zaidi, awe aliyekuwa mwaminifu kwa mume wake. Ni lazima ajulikane kwa mema aliyoyafanya: kulea watoto, kukaribisha wageni kwenye nyumba yake, kuwasaidia watu wa Mungu wenye uhitaji, wenye shida, na kutumia maisha yake kufanya wema wa aina zote. Lakini usiwaweke wajane wachanga katika orodha. Nguvu zao za mahitaji ya mwili zinawavuta wajiondea kwa Kristo, wanataka kuolewa tena. Kisha watahukumiwa kustahili adhabu kwa kutofanya walichoahidi kutenda hapo kwanza. Pia, wajane hawa vijana wanaanza kupoteza muda wao kwa kujihusisha na mambo ya watu wengine yasiyowahusu. Wanazungumzia mambo ambayo wasingepaswa kuzungumza. Hivyo nataka wajane vijana kuolewa, kuzaa watoto, na kutunza nyumba zao. Kama wakifanya hivi, adui yetu hatakuwa na sababu ya kutupinga kwa sababu yao. Lakini wajane wengine vijana wamegeuka na kumfuata Shetani. Kama yupo mwanamke aliyeamini aliye na wajane katika familia yake, ni lazima awatunze yeye mwenyewe. Ndipo Kanisa halitakuwa na mzigo wa kuwatunza hao bali kuwatunza ambao hawana mtu yeyote wa kuwasaidia. Wazee wanaoliongoza Kanisa katika njia nzuri wanapaswa kupokea heshima mara mbili; hasa wale wanaofanya kazi ya kuhubiri na kufundisha. Kama Maandiko yanavyosema, “Mnyama wa kazi akitumika kutenganisha ngano, usimzuie kula nafaka.” Na Maandiko pia yanasema, “Mfanyakazi anatakiwa kupewa ujira wake.” Usimsikilize yeyote anayemshitaki mzee. Unatakiwa kuwasikiliza tu kama wapo wawili au watatu ambao wanaweza kusema alichokosea mzee. Waambie wazee wanaotenda dhambi kwamba wana hatia, ufanye hivi mbele ya kanisa lote ili wengine wapate kuonywa. Mbele ya Mungu na Kristo Yesu na malaika walioteuliwa, nakuambia fanya hukumu hizo bila upendeleo. Mtendee kila mtu sawa sawa. Fikiri kwa makini kabla ya kuweka mikono yako juu ya yeyote kumfanya mzee. Usishiriki dhambi za wengine, na ujitunze uwe safi. Timotheo, acha kunywa maji tu, kunywa na kiasi kidogo cha mvinyo. Hii itakusaidia tumbo lako, na hutaugua mara kwa mara. Dhambi za watu wengine ni rahisi kuziona, hizo zinaonesha kwamba watahukumiwa. Lakini dhambi za wengine zitajulikana tu hapo baadaye. Inafanana na mambo mazuri wanayofanya watu. Zingine ni rahisi kuonekana. Lakini hata kama si dhahiri sasa, hakuna hata moja itakayojificha milele. Wote ambao ni watumwa waoneshe heshima kubwa kwa mabwana zao. Ndipo jina la Mungu na mafundisho yetu hayatakosolewa. Baadhi ya watumwa wanao mabwana ambao ni waamini, hivyo hao ni ndugu. Je, inamaanisha wasiwaheshimu mabwana zao? Hapana, watawatumikia hata kwa uzuri zaidi, kwa sababu wanawasaidia waaminio, watu wawapende. Haya ni mambo ambayo lazima uyafundishe na kumwambia kila mtu kufanya. Watu wengine wanafundisha uongo na hawakubaliani na mafundisho ya kweli ambayo yanatoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Hawakubali mafundisho ambayo yanatuongoza kumheshimu na kumpendeza Mungu. Wanajivunia wanayoyafahamu, lakini hawaelewi chochote. Wamepagawa na wana ugonjwa wa kupenda mabishano na mapigano ya maneno. Na hayo yanaleta wivu, ugomvi, matusi, na uovu wa kutoaminiana. Daima wanaleta shida, kwa sababu ni watu ambao kufikiri kwao kumeharibiwa. Wamepoteza ufahamu wao wa ukweli. Wanafikiri kwamba kujifanya wanamheshimu Mungu ni njia ya kupata utajiri. Kuishi kwa kumheshimu Mungu, hakika, ni njia ambayo watu hutajirika sana, kwa sababu inamaanisha wanaridhika na walivyo navyo. Tulipokuja ulimwenguni, tulikuja bila kitu, na tutakapokufa hatutachukua chochote. Hivyo, kama tukiwa na chakula na nguo, tutaridhika navyo. Watu ambao wanatamani kuwa matajiri wanajiletea majaribu wenyewe. Wananasa katika mtego. Wanaanza kutaka vitu vingi vya kijinga ambavyo vitawaumiza na kuwaharibu. Kupenda fedha kunasababisha aina zote za uovu. Watu wengine wamegeuka kutoka kwenye imani yetu kwa sababu wanataka kupata fedha nyingi zaidi. Lakini wamejisababishia wenyewe maumivu mengi na huzuni. Lakini wewe ni mali ya Mungu. Hivyo kaa mbali na mambo hayo yote, daima jaribu kutenda mema ili umheshimu Mungu na uwe na imani, upendo, uvumilivu, na upole. Tunatakiwa tupigane kutunza imani yetu. Jaribu kwa bidii kadri unavyoweza kushinda vita vya thawabu. Tunza uzima wa milele. Ni uzima mliyouchagua kuupata mlipoikiri imani yenu katika Yesu; huo ukweli wa ajabu mliousema waziwazi kwa wote kuusikia. Mbele ya Mungu na Kristo Yesu nakupa amri. Yesu ni yule aliyeshuhudia ukweli aliposimama mbele ya Pontio Pilato. Mungu ndiye anayetoa uhai kwa kila kitu. Nakuambia haya sasa: Tenda niliyokuamuru kufanya bila dosari au kulaumu mpaka muda atakapo rudi. Mungu atafanya hayo yatokee wakati utakapotimia. Yeye ni mwenye utukufu zaidi na mtawala pekee, mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana. Mungu pekee hafi, anaishi katika nuru angavu sana ambayo watu hawawezi kusogea karibu. Hakuna mtu aliyemwona Mungu; wala anayeweza kumuona. Heshima na nguvu ni zake milele. Amina. Wape amri hii wale ambao ni matajiri wa vitu vya ulimwengu huu. Waambie wasiwe na majivuno, bali wamtumaini Mungu wala si katika fedha zao. Fedha haziwezi kuaminiwa, lakini Mungu anatuhudumia kwa ukarimu mkubwa na anatupa vitu vyote ili tufurahi. Waambie wale ambao ni matajiri watende mema. Wawe matajiri katika kuzifanya kazi njema. Na uwambie wawe tayari kutoa na kuwapa wengine vitu. Kwa kufanya hivi, watajiwekea hazina kwa ajili yao wenyewe. Na hazina hiyo itakuwa ni msingi imara huo utakuwa msingi imara ambao maisha yao ya siku zijazo yatajengwa. Wataweza kuwa na maisha yaliyo ya kweli kabisa. Timotheo, Mungu ameweka vitu vingi kwako uvitunze. Uvitunze vyema. Jitenge na watu wanaosema mambo yasiyofaa ambayo hayatoki kwa Mungu na wale wanaokupinga na “elimu” ambayo siyo “elimu” kabisa. Watu wengine wanaodai kuwa na “elimu” wamepotea mbali kabisa kutokana na wanachoamini. Ninaomba neema ya Mungu iwe kwenu nyote. Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu. Ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alivyotaka. Yeye alinituma kwa sababu Mungu alipenda niwaeleze watu juu ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu. Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa: Neema, rehema na amani iwe kwako kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu. Daima namshukuru Mungu katika maombi yangu ninapokukumbuka usiku na mchana kwa ajili yako. Ni Mungu wa mababu zangu na daima nimemtumikia kwa dhamiri safi. Nikiyakumbuka machozi yako kwa ajili yangu, ninatamani kukuona, ili niweze kujazwa na furaha. Nimekumbuka imani yako ya kweli ambayo mwanzoni ilikuwa kwa bibi yako Loisi na kwa mama yako Eunike. Nami nashawishika hiyo iko kwako. Kwa sababu hii ninakukumbusha karama ya Mungu ambayo uliipokea wakati nilipokuwekea mikono. Sasa nataka uitumie karama hiyo na ikue zaidi na zaidi kama mwali wa moto mdogo uwakavyo ndani ya moto. Kwani Roho ambaye Mungu alitupa sisi ni chanzo cha ujasiri wetu, ni nguvu, upendo na fikra safi. Hivyo usione aibu kushuhudia juu ya Bwana wetu Yesu au kunionea aibu mimi, niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali aliteseka pamoja nami kwa ajili ya Habari Njema na Mungu hutupa nguvu. Alituokoa na kutuita katika maisha ya utakatifu, sio kwa sababu ya kitu cho chote tulichokifanya wenyewe, bali kwa kusudi lake mwenyewe na neema, ambayo ametupa sisi kwa Kristo Yesu kabla ya mwanzo wa wakati, na ambayo sasa imeonyeshwa kwetu kwa kuja kwake Kristo Yesu, Mwokozi wetu. Yeye Kristo aliiharibu mauti na kuleta uzima na kutokufa kwenye nuru kwa njia ya Habari Njema. Niliteuliwa na Mungu kutangaza Habari Njema kama mtume na mwalimu. Na ni kwa kazi hii ninateseka lakini sioni haya kwa sababu namjua yeye niliyemwekea imani yangu, na nina uhakika kuwa anaweza kukilinda kile nilichokikabidhi kwake hadi Siku ile. Yale uliyoyasikia nikiyafundisha yawe mfano kwako wa mafundisho utakayofundisha wewe. Uyafuate na yawe kielelezo cha mafundisho ya kweli na uzima kwa uaminifu na upendo ule ule ambao Kristo Yesu ametuonesha. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu anayeishi ndani yako, uyalinde mafundisho haya ya mazuri na yenye thamani mliyopewa dhamana kwayo. Unajua kwamba kila mtu aliyeko Asia ameniacha. Hata Figelo na Hermogene nao wameniacha. Ninaomba kwamba Bwana ataonesha rehema wa familia ya Onesiforo, amekuwa faraja yangu mara nyingi, na hakuona haya kwa ajili yangu kuwa gerezani. Kinyume chake, alipofika Rumi, alinitafuta kwa bidii hadi aliponiona. Bwana Yesu na amjalie kupata rehema kutoka kwa Bwana Mungu katika siku ile ya hukumu ya mwisho! Unafahamu vema ni kwa njia ngapi alinihudumia wakati nilipokuwa Efeso. Kwako wewe mwanangu, uwe hodari kwa njia ya neema inayopatikana kwa Kristo Yesu. Yachukue mambo uliyoyasikia kwangu mbele za mashahidi wengi, na yakabidhi kwa watu waaminifu ambao watakuwa na uwezo wa kuwafundisha wengine pia. Kama askari mwaminifu wa Kristo Yesu, jiunge nami katika mateso. Hakuna hata mmoja anayefanya kazi kama askari kisha akajishughulisha pia na mambo ya kiraia. Hii ni wa sababu anataka kumfurahisha kamanda wake. Na kama kuna mtu anayeshiriki katika mashindano ya riadha, hawezi kushinda taji endapo hatashindana kwa kufuata sheria. Mkulima mwenye juhudi anastahili kuwa wa kwanza kufurahia sehemu ya mavuno yake. Nakutaka wewe kuyafikiri ninayokuambia na Bwana atakupa uwezo wa kuyaelewa mambo haya yote. Endelea kumkumbuka Yesu Kristo, aliyefufuka kutoka kwa wafu, na ni kutoka ukoo wa Daudi. Na huu ndiyo Habari Njema ninayoihubiri. Kwa sababu ya Habari Njema ninateseka, hadi hatua ya kufungwa kwa minyororo kama mhalifu. Lakini ujumbe wa Mungu haujafungwa. Kwa hiyo nayavumilia yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili na wao waweze kuufikia wokovu unaopatikana katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Na hapa kuna usemi wa kuaminiwa: Kama tumekufa pamoja naye, tutaweza kuishi naye pia. Kama tutastahimili, tutaweza pia kumiliki pamoja naye. Kama tutamkana yeye, naye atatukana sisi. Kama hatutakuwa waaminifu, yeye anabaki kuwa mwaminifu, kwa sababu hawezi kujikana mwenyewe. Endelea kuwakumbusha watu juu ya mambo haya. Waonye kwa mamlaka mbele za Mungu wasipigane juu ya maneno. Mapigano hayo hayana mambo mazuri, bali huwaharibu wanaoyasikiliza. Jitahidi kujionesha mwenyewe kuwa umekubaliwa na Mungu, kama mtumishi asiye na kitu cho chote cha kumfadhaisha na anayeufanyia kazi ujumbe wa kweli ya Mungu katika njia sahihi. Bali uyaepuke majadiliano ya kijinga ya kidunia, ambayo huwapeleka watu mbali na Mungu, na mafundisho ya wale wanaoyachukua mafundisho hayo wanaenea kama saratani mwilini. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto, aliyeiasi na kuikosa kweli. Wanasema kuwa ufufuo kutoka kwa wafu kwa watu wote umekwisha kutokea, na wanageuza imani za watu wengine. Hata hivyo, msingi ulio imara ambao Mungu aliuweka unasimama imara, na maneno haya yameandikwa juu yake: “Bwana anawajua wale walio wake,” na “Kila anayesema kuwa ni wa Bwana aweze kuuacha ubaya.” Ndani ya nyumba kubwa hakuna vyombo vya dhahabu na fedha pekee, bali hata vya udongo na mbao. Na vingine ni vya kutumika kwa matukio maalumu, na vingine ni kwa matumizi ya kawaida. Hivyo mtu akitakaswa kutoka maovu yote, atakuwa mtakatifu na chombo maalumu cha kutumiwa na Bwana kilicho tayari kwa kila kazi njema. Bali uzikimbie tamaa za ujana na kuyatafuta maisha ya haki, imani, upendo na amani, pamoja na wote wanaomwita Bwana kwa mioyo safi. Nyakati zote ujiepushe na mabishano ya kijinga, kwa sababu unajua kuwa huleta mabishano makubwa. Kwani mtumwa wa Bwana hapaswi kubishana, bali kuwa mkarimu kwa watu wote, mwenye ujuzi katika kufundisha na asiye mtukanaji. Anapaswa kuwaelekeza wapinzani wake kwa upole katika tumaini kwamba Mungu anaweza kuwasaidia hao kutubu na kuujua ukweli, na ili waweze kurudi katika fahamu zao na kuuepuka mtego wa adui, ambako wameshikiliwa kama mateka na Ibilisi na wamelazimishwa kuyafanya mapenzi yake. Kumbuka hili: Katika siku za mwisho nyakati ngumu zitakuja. Watu watajipenda wenyewe na kupenda fedha. Watakuwa na majivuno na wenye jeuri. Watawatukana wengine kwa matusi. Hawatawatii wazazi wao. Watakuwa wasio na shukrani. Watapinga kila kinachompendeza Mungu. Hawatakuwa na upendo kwa wengine na hawatakubali kuwasamehe wengine. Watawasingizia wengine na hawataweza kujizuia. Watakuwa wakatili na watayachukia yaliyo mema. Watu watawasaliti rafiki zao. Watafanya mambo ya kipuuzi bila kufikiri na watajisifu wenyewe. Badala ya kumpenda Mungu watapenda starehe. Watajifanya kuwa wanamheshimu Mungu, lakini watazikana nguvu za uzima ambazo ndizo zinazotuwezesha kwa hakika kumpa utukufu na kumpendeza. Ukae mbali na watu wa jinsi hiyo. Nasema hivi kwa sababu baadhi yao wanaziendea nyumba na kuwateka wanawake dhaifu, waliolemewa na dhambi na kuvutwa na kila aina ya tamaa. Wanawake hawa nyakati zote wanataka kujifunza, lakini hawawezi kamwe kuufikia ufahamu wote wa kweli. Kama ambavyo Yane na Yambre walivyompinga Musa, ndivyo hata watu hawa wanavyoipinga kweli. Ni watu ambao akili zao zimeharibika, nao wameshindwa kuifuata imani. Lakini hawataendelea mbele zaidi, kwa sababu upumbavu wao utadhihirika wazi wazi kwa watu wote, kama ujinga wa Yane na Yambre ulivyojulikana. Ninyi hata hivyo mmeyazingatia na kuyashika mafundisho yangu, mwenendo wangu na kusudi langu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu na ustahimilivu wangu, mateso yangu na taabu zangu. Mnayajua mambo yaliyonitokea kule Antiokia, Ikonia, na Listra, mateso ya kutisha niliyoyastahimili! Lakini Bwana akaniokoa kutoka katika hayo yote. Kwa hakika wote wanaoishi maisha yenye kumtukuza Mungu kama wafuasi wa Kristo Yesu watasumbuliwa. Lakini watu waovu na wanaodanganya wengine wataendelea kuwa wabaya zaidi. Watawadaganya wengine na wao pia watajidanganya wenyewe. Lakini imekupasa wewe kuendelea kuyashika mambo yale uliyojifunza na kuyathibitisha moyoni mwako kuwa ni ya kweli. Wewe unawajua na unawaamini wale waliokufundisha. Na unajua kwamba umeyajua Maandiko Matakatifu tangu ukiwa mtoto. Maandiko hayo yana uwezo wa kukupa hekima. Hekima hiyo itakuongoza hadi kwenye wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maandiko yote tumepewa na Mungu. Na maandiko yote yanafaa kwa mafundisho kwa kusudi la kuwaonesha watu makosa yao na kuwafundisha njia sahihi ya kuishi ili mtu anayemtumikia Mungu aweze kuandaliwa na kukamilishwa kwa ajili ya kufanya kila kazi njema. Nakuamuru mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, ambaye punde atawahukumu wale walio hai na wale waliokwisha kufa na juu ya kuja kwa mara ya pili kwa Kristo kwa sababu kwa hakika atatokea kuja kutawala kama Mfalme: Hubiri Ujumbe, uwe tayari kutimiza wajibu wako wakati ulio sahihi hata ule usio sahihi. Wathibitishie watu kwa wanafanya makosa na uwaonye juu ya yale yatakayowatokea. Ufanye hivi kwa subira kubwa na tahadhari katika yale unayofundisha. Nasema hivi kwa sababu utakuja wakati ambapo watu hawatakuwa tayari kuyasikiliza mafundisho yenye uzima. Badala yake watawatafuta walimu wanaowapendeza. Watawatafuta walimu wanaosema yale wanayotaka kusikia. Na watayageuzia mbali masikio yao kutoka kwenye kweli na kugeukia simulizi za uongo. Lakini wewe ujizuie mwenyewe katika mambo yote; vumilia mateso; fanya kazi ya mhubiri wa Habari Njema; ifanye huduma uliyopewa na Mungu. Kwangu mimi, nimemiminwa kama kinywaji cha sadaka, na wakati wa kuondoka kwangu kutoka katika maisha haya umekwisha kufika. Nimejihusisha katika mashindano ya thamani; nimemaliza mbio; nimeilinda imani. Sasa tuzo ya mshindi inaningoja, hii ni taji inatolewa kwa wenye haki. Bwana, aliye hakimu wa haki atanipa taji hiyo katika Siku ile. Ndio atanipa mimi na yeyote mwingine anayengojea kwa dhati kuja kwake. Jitahidi kuja kuniona mapema uwezavyo, kwani Dema aliniacha kwa sababu aliupenda ulimwengu wa sasa na ameenda Thesalonike. Kreske ameenda Galatia, na Tito ameenda Dalmatia. Luka ni peke yake aliyebaki nami. Mchukue Marko na uje naye utakapokuja, kwa sababu anaweza kunisaidia katika kazi yangu. Namtuma Tikiko kule Efeso. Utakapokuja njoo na koti nililoliacha katika nyumba ya Karpo kule Troa. Pia uniletee vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi. Iskanda aliye mfua vyuma amenitendea mabaya mengi. Bwana atamlipa kwa yale aliyotenda. Wewe pia uwe mwangalifu kwake, kwa kuwa ameyapinga kwa juhudi mafundisho yetu. Mara ya kwanza nilipokuwa nafanya utetezi wangu, hakuna hata mmoja aliyekuja kunisaidia. Badala yake wote wakaniacha. Na wasihesabiwe hayo na Mungu. Lakini Bwana akasimama upande wangu na kunitia nguvu, ili ujumbe uweze kunenwa nami kwa ukamilifu ili kwamba Mataifa wote waweze kusikia. Na nikaokolewa kutoka katika mdomo wa simba. Bwana ataniokoa kutokana na kila mashambulizi maovu na atanileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Utukufu uwe wake milele na milele. Amina. Msalimu Priska na Akila na wale wa nyumbani mwake Onesiforo. Erasto alibaki Korintho. Nilimwacha Trofimo kule Mileto kwa sababu alikuwa mgonjwa. Jitahidi kuja kabla ya msimu wa baridi. Ebulo anakusalimu, na Pude, Lino, na Klaudia, na ndugu na dada wote. Bwana awe nawe. Neema ya Mungu iwe nanyi. Salamu kutoka kwa Paulo, mtumwa wa Mungu na mtume aliyetumwa na Yesu Kristo. Kazi yangu ni kuwasaidia wateule wa Mungu kumwamini Yeye zaidi na kuyaelewa kwa kina mafundisho ya Kristo. Mafundisho haya yatawaongoza kuishi katika njia inayomtukuza na kumpendeza Mungu. Na kisha wakatarajie kuishi pamoja na Mungu milele. Kabla ya mwanzo wa ulimwengu, Mungu aliahidi uzima wa milele kwa watu wake. Na wakati sahihi ulipotimia aliidhihirisha ile habari njema. Ujumbe huo ulikabidhiwa kwangu kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu kumwambia kila mtu. Nakuandikia wewe Tito, mwanangu halisi katika imani tunayoshiriki: Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu iwe nanyi. Nilikuacha kule Krete ili uweze kuyakamilisha yale yaliyokuwa yamebaki kufanyiwa kazi. Kisha nakuagiza uteue wazee na kuwaweka kuwa viongozi katika kila mji. Anayeweza kuteuliwa ni yule ambaye halaumiwi kwa matendo yoyote mabaya, na aliye mwaminifu kwa mkewe, na anao watoto wanaoamini Mungu na ambao sio wakaidi. Kwa sababu kila askofu, anao wajibu wa kuitunza kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiyelaumiwa kwa kutenda mabaya yoyote. Asiwe mtu mkorofi. Asiwe mtu aliye mwepesi wa hasira. Asiwe mgomvi. Asiwe mtu mwenye kujipatia fedha toka kwa watu kwa njia ya udanganyifu. Mzee anapaswa kuwa mtu anayewakaribisha watu nyumbani mwake. Anapaswa kuyapenda yaliyo mema. Azingatie kuishi maisha yaliyo matakatifu. Na awe na uwezo wa kudhibiti nafsi yake. Anapaswa kuwa mwaminifu kwa ujumbe ule ule wa kweli tunaofundisha. Kwa namna hiyo ataweza kuwatia moyo wengine kwa mafundisho ya kweli na yenye manufaa. Na ataweza kuwathibitishia wale wanaopinga mafundisho yake ya kuwa hawako sahihi. Aina hii ya mafundisho ni muhimu kwa sababu wako watu wengi wasiopenda kumsikiliza mtu yeyote. Hao wanazungumzia mambo yao wenyewe yasiyo ya maana na kuwapotosha wengine waiache kweli. Ninaongelea hasa baadhi ya Wayahudi waaminio. Ni lazima wanyamazishwe kwani wanaivuruga jamii nzima kwa kufundisha mambo ambayo wasingepaswa kuyafundisha, lakini wanafanya hivyo ili kujipatia mapato yasiyo ya uaminifu! Mmoja miongoni mwa watu wa kwao, Nabii kutoka Krete, alisema: “Wakrete ni waongo daima. Si bora kuliko wanyama wa porini. Daima wapo tayari kula, lakini hawapendi kufanya kazi.” Usemi huu ni kweli, kwa hivyo wakaripie vikali ili wawe imara katika imani yao na wasiendelee kuzisikilliza simulizi zinazopotosha za Kiyahudi na amri za wanadamu walioiacha kweli. Kwa wale watu wenye mawazo yaliyo safi, kila kitu ni safi. Lakini hakuna kinachoweza kuwa safi kwa wasioamini ambao dhambi zao zimewafanya kuwa wachafu. Mawazo yao daima huwa yasiyo haki, na dhamiri zao pia zimekuwa chafu. Hao hudai kuwa wanamjua Mungu, lakini matendo yao maovu yanaonesha kwa hakika kuwa hawamjui. Ni watu wenye kuchukiza mno na wasiotii, na hawafai kwa lo lote lililo jema. Lakini wewe Tito daima uwaambie waaminio mambo yanayokubaliana na mafundisho ya kweli na yenye uzima. Wanaume wazee wanapaswa kuwa na kiasi na kufanya mambo yenye kuleta heshima. Wanapaswa kuwa na busara katika maisha yao. Kuwa na nguvu katika imani kwa Mungu, upendo kwa wengine, na uvumilivu. Vivyo hivyo wafundishe wanawake wazee wawe na mwenendo mzuri. Wafundishe wasiwe wachochezi na wasiwe watumwa wa mvinyo. Wanapaswa kufundisha yale yaliyo mema. Kwa jinsi hiyo wataweza kuwakumbusha wanawake vijana jinsi wanavyopaswa kuishi. Wanawake vijana wanapaswa kuwaonesha upendo waume zao na kuwapenda watoto wao. Wanapaswa kuwa na busara na wasafi kiroho, wakizitunza nyumba zao, kuwa wakarimu, na kuwa tayari kuwatumikia waume zao wenyewe, ili asiwepo atakayeudharau ujumbe wa Neno la Mungu. Kadhalika endelea kuwahimiza wanaume vijana kuwa na busara. Katika kila kitu ujioneshe kuwa wewe ni mfano wa matendo mema. Katika mafundisho yako onesha kuwa una moyo safi na uko makini. Ufundishe kile ambacho ni sahihi kwa wazi, ili asiwepo yeyote atakayepinga mafundisho yako. Tumia mazuri ambayo hayatasemwa vibaya ili wale wanaokupinga waaibishwe kwa ajili ya kukosa lo lote baya la kusema dhidi yetu. Wafundishe watumwa kuwatii bwana zao katika kila jambo, wajitahidi kuwapendeza na sio kubishana nao wala kwa siri wasiwaibie bali waudhihirishe uaminifu kamili, ili katika mambo yote wayapatie sifa njema mafundisho kutoka kwa Mungu, Mwokozi wetu. Maana Mungu ameidhihirisha neema yake inayookoa kwa watu wote. Hiyo inatufundisha kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia ili tuishi katika ulimwengu wa sasa kwa njia ya werevu, haki na kuionesha heshima yetu kwa Mungu, kadri tunavyosubiri ile Siku iliyobarikiwa tunayoitumaini ambapo utukufu wa Mungu wetu mkuu na Mwokozi Yesu Kristo itakapofunuliwa. Alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili aweze kutuweka huru sisi kutoka katika uovu wote na kuweza kutusafisha kwa ajili yake watu walio wake mwenyewe, wale walio na shauku ya kufanya matendo mema. Endelea kufundisha ukihimiza na kukemea kuhusu mambo haya, na fanya hivyo kwa mamlaka yote, na mtu yeyote asikudharau. Uwakumbushe watu wako ya kuwa wanapaswa kujiweka chini ya mamlaka ya watawala wao na uongozi wa dola. Wanapaswa kuwatii viongozi hao na kuwa tayari kufanya kila jema wanaloweza. Waambie hawapaswi kumtukana mtu yeyote, bali wawe wema na wapole kwa watu wote. Hapo zamani hata sisi tulikuwa wajinga, wakaidi na tulidanganyika. Tulikuwa watumwa kwa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu. Tulichukiwa na watu nasi tukachukiana wenyewe kwa wenyewe. Lakini Mungu Mwokozi wetu alitudhihirishia wema na upendo alionao kwa wanadamu. Alituokoa kwa sababu yeye ni mwenye rehema, siyo kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda na kupata kibali chake, bali ni kwa rehema yake. Yeye aliziosha dhambi zetu, akatupa maisha mapya kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ikawa kama kuzaliwa kwa mara ya pili. Mungu ametumiminia Roho Mtakatifu kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu. Kwa neema yake Mungu alituweka huru mbali na dhambi. Akatufanya kuwa warithi wake tulio na tumaini la uzima wa milele. Huu ni usemi wa kuaminiwa. Nawataka ninyi kuyasisitiza mambo haya, ili wale waliokwisha kumwamini Mungu waweze kujitoa katika matendo mema. Mambo haya ni mazuri na ya kuwanufaisha watu. Lakini yaepuke mabishano ya kipumbavu, majadiliano kuhusu koo, mabishano na ugomvi kuhusu Sheria, maana hayana faida na hayafai. Mwepuke mtu anayesababisha matengano baada ya onyo la kwanza na la pili, kwa sababu unajua kuwa mtu wa jinsi hiyo amepotoka na anatenda dhambi. Amejihukumu mwenyewe. Nilipomtuma kwako Artema au Tikiko, jitahidi kuja Nikopoli ili kuonana nami, kwa sababu nimeamua kukaa huko wakati wa msimu wa baridi. Jitahidi kumsaidia mwanasheria Zena pamoja na Apolo kwa lo lote watakalohitaji kwa ajili ya safari yao, ili wasipungukiwe na kitu cho chote. Watu wetu wanapaswa kujifunza kujihusisha katika kutenda mema ili kusaidia kukitokea mahitaji, ili wasiwe watu wasiokuwa na manufaa. Wote nilio pamoja nami wanakusalimu. Uwasalimu wote wanaotupenda katika imani. Neema ya Mungu iwe nanyi nyote. Kutoka kwa Paulo mfungwa kwa kusudi la Kristo Yesu, na kutoka kwa Timotheo ndugu yetu. Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtenda kazi pamoja nasi; kwa Afia dada yetu, Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa linalokutania nyumbani mwako. Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo ziwe pamoja nawe. Namshukuru Mungu wangu siku zote kila ninapokukumbuka katika maombi yangu, kwa sababu nasikia juu ya upendo na uaminifu ulionao katika Bwana Yesu na unaouonesha kwa watu wa Mungu. Ninaomba kwamba ile imani unayoishiriki pamoja nasi ikusaidie wewe kuelewa kila fursa tulio nayo ya kutenda mema kama wale tunaomwamini Kristo. Nimepokea furaha kubwa na faraja kutokana na upendo wako, kwa sababu mioyo ya watu wa Mungu imepata nguvu mpya kwa juhudi zako ndugu yangu. Hivyo hiyo ndiyo sababu nakuagiza wewe kufanya jambo unalopaswa kulifanya. Kwa mamlaka niliyo nayo katika Kristo naweza kukuamuru kufanya hilo. Lakini sikuamuru; bali kwa sababu ya upendo nakusihi ufanye hivyo. Mimi Paulo, niliye mzee wa umri sasa, na sasa mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu. Ninakusihi kuhusu mwanangu Onesimo niliyemleta katika maisha mapya tulio nayo katika Bwana nilipokuwa gerezani. Huyo ambaye siku za nyuma hakuwa wa manufaa kwako, lakini sasa anafaa sio kwako tu bali hata kwangu mimi. Ninamrudisha kwako, kitu ambacho kimekuwa kigumu sawa na kuupoteza moyo wangu. Ningetamani kuendelea kuwa naye hapa, ili aendelee kunihudumia kwa niaba yako nitakapokuwa bado gerezani kwa ajili ya Habari Njema. Lakini sikuwa tayari kufanya jambo lo lote bila ruhusa yako, ili kila jambo lako zuri litendeke bila lazima bali kwa hiari yako mwenyewe. Labda sababu ya Onesimo kutenganishwa nawe kwa kipindi kifupi ni kuwezesha muwe pamoja siku zote, si mtumwa tena, bali ni zaidi ya mtumwa; kama ndugu mpendwa. Nampenda sana lakini wewe utampenda zaidi, sio tu kama kaka katika familia yenu, bali pia kama mmoja wa walio katika familia ya Bwana. Ikiwa unanitambua mimi kama niliye mwenye imani moja nawe, basi mpokee Onesimo na umkubali kama vile ambavyo ungenikubali. Endapo amekukosea jambo lo lote au unamdai kitu cho chote, unidai mimi badala yake. Mimi Paulo naandika kwa mkono wangu mwenyewe ya kwamba nitakulipa. Tena sina sababu ya kukumbusha kuwa una deni kwangu juu ya maisha yako. Kwa hiyo kaka yangu, kama mfuasi wa Bwana, tafadhali nipe upendeleo katika hili. Ndipo itakuwa faraja kuu kwangu kama kaka yako katika Kristo. Ninapokuandikia barua hii nina ujasiri mkubwa kwamba utakubaliana nami na najua kwamba utafanya zaidi ya haya ninayokuomba. Pamoja na hayo naomba uniandalie chumba cha kufikia, kwa sababu nina matumaini kwamba kwa maombi yenu nitaachiliwa na kuletwa kwenu. Epafra mfungwa pamoja nami katika Kristo Yesu anakusalimu. Marko, Aristarko, Dema, na Luka watendakazi pamoja nami nao wanakusalimu. Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja nanyi. Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa kuwatumia manabii. Alisema nao mara nyingi na kwa njia nyingi tofauti. Lakini sasa katika siku hizi za mwisho Mungu amesema nasi tena kupitia Mwana wake. Mungu aliuumba ulimwengu wote kupitia Mwana wake. Na alimchagua Mwana kumiliki mambo yote. Huyo Mwana huuonesha utukufu wa Mungu. Yeye ni nakala halisi ya asili yake Mungu, na huviunganisha vitu vyote pamoja kwa amri yake yenye nguvu. Mwana aliwasafisha watu kutoka katika dhambi zao. Kisha akaketi upande wa kuume wa Mungu, aliye Mkuu huko Mbinguni. Mwana akawa mkuu zaidi kuliko malaika, na Mungu akampa jina lililo kuu zaidi kuliko lolote katika majina yao. Mungu kamwe hajamwambia malaika yeyote maneno haya: “Wewe ni Mwanangu. Mimi leo hii nimekuwa Baba yako.” Mungu pia kamwe hajasema juu ya malaika, “Nitakuwa Baba yake, naye atakuwa mwanangu.” Na kisha, pale Mungu anapomtambulisha Mwanaye mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, anasema, “Basi malaika wote wa Mungu wamwabudu yeye.” Hivi ndivyo Mungu alivyosema kuhusu malaika: “Yeye huwabadilisha malaika zake kuwa upepo na watumishi wake kuwa miali ya moto.” Lakini hivi ndivyo alivyosema kuhusu Mwana wake: “Mungu, ufalme wako utadumu milele na milele. Unatumia mamlaka yako kwa haki. Unapenda kilicho sahihi na kuchukia kilicho na makosa. Hivyo Mungu, Mungu wako, amekuchagua wewe, na amekupa heshima na furaha zaidi kupita yeyote aliye kama wewe.” Pia Mungu alisema, “Ee Bwana, mwanzo uliiumba dunia, na mikono yako ikaliumba anga. Vitu hivi vitatoweka, lakini wewe utaendelea kuwepo. Vyote vitachakaa kama mavazi makuu kuu. Utavikunja hivyo kama koti, navyo vitabadilishwa kama mavazi. Lakini wewe hubadiliki, na uhai wako hautafikia mwisho.” Na Mungu hakuwahi kusema haya kwa malaika: “Ukae mkono wangu wa kuume hadi nitakapowaweka adui zako chini ya uwezo wako.” Malaika wote ni roho ambao humtumikia Mungu nao hutumwa kuwasaidia wale watakaoupokea wokovu. Hivyo tunapaswa kuwa makini zaidi kuzingatia yale tuliyofundishwa. Tunapaswa kuwa makini ili tusiondolewe polepole kutoka katika njia iliyo ya kweli. Fundisho kwamba Mungu alizungumza kupitia malaika limedhihirishwa kuwa ni la kweli. Na kila mara watu wake walipotenda jambo kinyume na fundisho lake, waliadhibiwa kwa yale waliyofanya. Waliadhibiwa walipoacha kutii fundisho hilo. Hivyo kwa hakika hata nasi tutaadhibiwa kama hatutauzingatia wokovu mkuu tulionao. Alikuwa ni Bwana Yesu aliyewaambia watu kwa mara ya kwanza juu ya wokovu huo. Na wale waliomsikiliza walithibitisha kwetu kuwa yale mambo yalikuwa ni kweli. Mungu alithibitisha hayo pia kwa kutumia ishara, maajabu, na aina zingine zote za miujiza. Na alithibitisha hayo kwa kuwapa watu vipawa tofauti kwa njia ya Roho Mtakatifu kwa namna ile aliyotaka. Mungu hakuwachagua malaika wawe watawala juu ya ulimwengu mpya unaokuja. Ulimwengu huo ujao ni ndiyo ambao tumekuwa tukiuzungumzia. Imeandikwa mahali fulani katika Maandiko: “Kwa nini watu ni muhimu sana kwako? Kwa nini hata unafikiri juu yao? Kwa nini unamjali mwana wa mwanadamu? Je, yeye ni muhimu kiasi hicho? Kwa muda mfupi ulimfanya awe chini kuliko malaika. Ukamvisha taji yenye utukufu na heshima. Ukaweka kila kitu chini ya udhibiti wake.” Kama Mungu aliweka vitu vyote chini ya udhibiti wake, basi hakikuwepo chochote kilichoachwa ambacho hakukitawala. Lakini bado hatujamwona akitawala juu ya vyote. Kwa kipindi kifupi Yesu aliwekwa chini kuliko malaika, lakini sasa tunamwona akiwa amevaa taji ya utukufu na heshima kwa sababu aliteseka na kufa. Kwa sababu ya neema ya Mungu, Yesu alikufa kwa ajili ya kila mmoja. Mungu aliyeumba vitu vyote na ambaye kwa utukufu wake vitu vyote vipo; alitaka watu wengi wawe watoto wake na kuushiriki utukufu wake. Hivyo alifanya yale aliyohitaji kuyafanya. Alimkamilisha yeye anayewaongoza watu hao kuuelekea wokovu. Kwa njia ya mateso yake Mungu alimfanya Yesu kuwa Mwokozi mkamilifu. Yesu, ambaye anawafanya watu kuwa watakatifu, na wale wanaofanywa kuwa watakatifu wanatoka katika familia moja. Hivyo haoni aibu kuwaita kaka na dada zake. Anasema, “Mungu, nitawaeleza kaka na dada zangu habari zako. Mbele za watu wako wote nitaziimba sifa zako.” Pia anasema, “Nitamwamini Mungu.” Na pia anasema, “Nipo hapa, na pamoja ni wapo watoto niliopewa na Mungu.” Watoto hawa ni watu walio na miili ya damu na nyama. Hivyo Yesu mwenyewe akawa kama wao na akapata uzoefu ule ule waliokuwa nao. Yesu alifanya hivi ili, kwa kufa kwake, aweze kumharibu yeye aliye na nguvu ya mauti, Ibilisi. Yesu akawa kama watu hawa na akafa ili aweze kuwaweka huru. Walikuwa kama watumwa maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa kwao kifo. Kwa uwazi, siyo malaika ambao Yesu huwasaidia. Yeye huwasaidia watu waliotoka kwa Ibrahimu. Kwa sababu hii, Yesu alifanyika kama sisi, kaka na dada zake kwa kila namna. Akawa kama sisi ili aweze kuhudumu kwa niaba yetu mbele za Mungu wa kuhani mkuu aliye mwaminifu na mwenye rehema. Ndipo angetoa sadaka ya kuziondoa dhambi za watu. Na sasa anaweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa. Yuko radhi kuwasaidia kwa sababu yeye mwenyewe aliteseka na alijaribiwa. Hivyo, kaka na dada zangu, ninyi mliochaguliwa na Mungu muwe watu wake watakatifu, mfikirieni Yesu. Yeye ndiye tunayeamini kuwa Mungu alimtuma kuja kutuokoa na awe kuhani wetu mkuu. Mungu akamfanya kuhani wetu mkuu, naye akawa mwaminifu kwa Mungu kama Musa alivyokuwa. Naye alifanya kila kitu ambacho Mungu alimtaka akifanye katika nyumba ya Mungu. Mtu anapojenga nyumba, watu watamheshimu mjenzi zaidi kuliko ile nyumba. Ndivyo ilivyo kwa Yesu. Anastahili heshima kubwa kuliko Musa. Kila nyumba huwa imejengwa na mtu fulani, lakini Mungu alijenga kila kitu. Musa alikuwa mwaminifu kama mtumishi katika nyumba yote ya Mungu. Aliwajulisha watu yale ambayo Mungu angeyasema katika siku zijazo. Lakini Kristo ni mwaminifu katika kuitawala nyumba ya Mungu kama Mwana. Nasi tu nyumba ya Mungu, kama tukibaki wajasiri katika tumaini kuu tunalofurahia kusema kuwa tunalo. Ni kama vile anavyosema Roho Mtakatifu: “Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu, msiifanye migumu mioyo yenu kama hapo zamani, mlipomgeuka Mungu. Hiyo ndiyo siku ulipomjaribu Mungu mle jangwani. Kwa miaka 40 jangwani, watu wako wakaona niliyoyatenda. Lakini walinijaribu na ustahimilivu wangu. Hivyo nikawakasirikia. Nikasema, ‘Mawazo yao siku zote hayako sahihi. Hawajawahi kamwe kuzielewa njia zangu.’ Hivyo nilikasirika na kuweka ahadi: ‘Kamwe hawataingia katika sehemu yangu ya pumziko.’” Hivyo ndugu na dada, muwe makini ili asiwepo miongoni mwenu atakayekuwa na mawazo maovu yanayosababisha mashaka mengi ya kuwafanya muache kumfuata Mungu aliye hai. Bali mhimizane ninyi kwa ninyi kila siku, maadamu mna kitu kinachoitwa “leo.” Msaidiane ninyi kwa ninyi ili asiwepo miongoni mwenu atakayedanganywa na dhambi akawa mgumu sana kubadilika. Tunayo heshima ya kushirikishana katika yote aliyo nayo Kristo endapo tutaendelea hadi mwisho kuwa na imani ya uhakika tuliyokuwa nayo mwanzoni. Ndiyo sababu Roho anasema: “Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu, msiifanye migumu mioyo yenu kama hapo zamani, wakati mlipogeuka mbali na Mungu.” Ni nani hawa walioisikia sauti ya Mungu na kugeuka kinyume naye? Walikuwa watu wote ambao Musa aliwaongoza kutoka Misri. Na ni kina nani waliokasirikiwa na Mungu kwa miaka 40? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi. Na maiti zao zikaachwa jangwani. Na ni watu gani ambao Mungu alikuwa akisema nao alipotoa ahadi kuwa kamwe wasingeingia mahali penye mapumziko? Alikuwa anazungumza nao ambao hawakumtii. Hivyo tunaona kuwa hawakuruhusiwa kuingia na kupata pumziko la Mungu, kwa sababu hawakuamini. Na bado tunayo ahadi ambayo Mungu aliwapa watu wake. Ahadi hiyo ni kwamba tuweze kuingia katika sehemu ya pumziko. Hivyo tunapaswa kuwa waangalifu ili asiwepo atakayeikosa ahadi hiyo. Ndiyo, habari njema kuhusu hilo zilielezwa kwetu kama ilivyokuwa kwao. Lakini ujumbe waliousikia haukuwasaidia. Waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani. Ni sisi tu tunaoamini tunaoweza kuingia katika sehemu ya pumziko ya Mungu. Kama Mungu alivyosema: “Nilikasirika na nikaweka ahadi: ‘Hawataingia kamwe kwenye sehemu yangu ya pumziko.’” Lakini kazi ya Mungu ilikamilika tangu wakati ule alipoumba ulimwengu. Ndiyo, mahali fulani katika Maandiko alizungumza juu ya siku ya saba ya juma. Alisema, “Hivyo katika siku ya saba, Mungu alipumzika kazi zake zote.” Lakini katika Maandiko ya hapo juu Mungu alisema, “Hawataingia kamwe katika sehemu yangu ya pumziko.” Hivyo fursa bado ipo kwa baadhi kuingia na kufurahia pumziko la Mungu. Lakini waliosikia kwanza habari njema juu yake hawakuweza kuingia, kwa sababu hawakutii. Hivyo Mungu akapanga siku nyingine maalumu. Inaitwa “leo.” Alizungumza juu ya siku hiyo kupitia kwa Daudi siku nyingi zilizopita kutumia maneno tuliyonukuu mwanzoni: “Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu, msiifanye migumu mioyo yenu.” Tunajua kuwa Yoshua hakuwaongoza watu hadi sehemu ya pumziko ambayo Mungu aliwaahidi. Tunalijua hili kwa sababu Mungu alisema baadaye kuhusu siku ya pumziko. Hii inaonesha kuwa pumziko la siku ya saba kwa watu wa Mungu bado linakuja. Mungu alipumzika alipokamilisha kazi yake. Hivyo kila mmoja anayeingia katika sehemu ya pumziko ya Mungu vilevile atapata pumziko kutoka katika kazi yake kama Mungu alivyofanya. Hivyo hebu na tujitahidi tuwezavyo kuingia katika sehemu ya pumziko ya Mungu. Tunapaswa kujitahidi ili asiwepo miongoni mwetu atakayepotea kwa kufuata mfano wa wale waliokataa kumtii Mungu. Neno la Mungu liko hai na linatenda kazi. Lina ukali kupita upanga ulio na makali sana na hukata hadi ndani yetu. Hukata ndani hadi sehemu ambayo nafsi na roho huwa zimeunganishwa pamoja. Neno la Mungu hukata hadi katikati ya maungio na mifupa yetu. Linahukumu mawazo na hisia ndani ya mioyo yetu. Hakuna chochote ulimwenguni mwote kinachoweza kufichika mbele za Mungu. Anaweza kuviona vitu vyote kwa uwazi kabisa. Kila kitu kiko wazi mbele zake. Na kwake tutapaswa kujieleza jinsi tulivyoishi. Tunaye kuhani mkuu sana ambaye ameenda kuishi na Mungu kule mbinguni. Yeye ni Yesu Mwana wa Mungu. Hivyo tuendelee kuitamka imani yetu katika yeye. Yesu, kuhani wetu mkuu, anaweza kuuelewa udhaifu wetu. Yesu alipoishi duniani, alijaribiwa katika kila njia. Alijaribiwa kwa njia hizo hizo tunazojaribiwa, lakini hakutenda dhambi. Tukiwa na Yesu kama kuhani wetu mkuu, tunaweza kujisikia huru kuja mbele za kiti cha enzi cha Mungu ambako kuna neema. Hapo tunapata rehema na neema ya kutusaidia tunapokuwa tunahitaji. Kila kuhani Mkuu wa Kiyahudi alichaguliwa kutoka miongoni mwa watu. Kuhani huyo anapewa kazi ya kuwasaidia watu katika mambo wanayopaswa kumfanyia Mungu. Anapaswa kumtolea Mungu sadaka na sadaka za dhambi. Kuhani mkuu anao udhaifu wake binafsi. Hivyo anapaswa kuwa mpole kwa wale wanaokosea kwa sababu ya kutokujua. Hutoa sadaka kwa ajili ya dhambi zao, lakini kutokana na udhaifu wake anapaswa pia kutoa sadaka kwa ajili dhambi zake mwenyewe. Kuwa kuhani mkuu ni heshima. Lakini hayupo anayejichagua mwenyewe kwa ajili ya kazi hii. Mtu huyo anapaswa kuwa amechaguliwa na Mungu kama alivyokuwa Haruni. Ndivyo ilivyo hata kwa Kristo. Hakujichagua mwenyewe kuwa na heshima na kuwa kuhani mkuu. Lakini Mungu alimchagua. Mungu akamwambia: “Wewe ni mwanangu. Leo nimekuwa baba yako.” Na katika sehemu nyingine ya Maandiko Mungu anasema: “Wewe ni kuhani mkuu milele; kama Melkizedeki alivyokuwa kuhani.” Yesu alipoishi duniani alimwomba Mungu, akiusihi msaada kutoka kwa yule anayeweza kumwokoa kutoka mauti. Alimwomba Mungu kwa sauti kuu na kwa machozi. Na Mungu alizisikia sala zake kwa sababu ya heshima yake kuu kwa Mungu. Yesu alikuwa mwana wa Mungu, lakini aliteseka, na kwa njia ya mateso yake alijifunza kutii chochote alichosema Mungu. Hili lilimfanya yeye awe kuhani mkuu mkamilifu, anayetoa njia kwa ajili ya kila mmoja anayemtii ili kuokolewa milele. Mungu alimfanya yeye kuhani mkuu, kama alivyokuwa Melkizedeki. Tunayo mambo mengi ya kuwaeleza kuhusu hili. Lakini ni vigumu kufafanua kwa sababu mmeoteza shauku ya kusikiliza. Mmekuwa na muda wa kutosha ambapo sasa mngepaswa kuwa walimu. Lakini mnahitaji mtu awafundishe tena mafundisho ya Mungu ya mwanzo. Bado mnahitaji mafundisho ambayo yako kama maziwa. Hamjafikia kiwango cha chakula kigumu. Yeyote anayeishi kwa kutegemea maziwa tu bado ni mtoto mchanga, hayupo tayari kuelewa zaidi kuhusu kuishi kwa haki. Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu ambao wamekua. Kutokana na uzoefu wao wamejifunza kuona tofauti baina ya jema na ovu. Hivyo tusiendelee tena na masomo ya msingi juu ya Kristo. Tusiendelee kurudia kule tulikoanzia. Tuliyaanza maisha yetu mapya kwa kugeuka kutoka katika uovu tuliotenda zamani na kwa kumwamini Mungu. Hapo ndipo tulipofundishwa kuhusu mabatizo, kuwawekea watu mikono, ufufuo wa wale waliokwisha kufa, na hukumu ya mwisho. Sasa tunahitajika kuendelea mbele hadi kwenye mafundisho ya ukomavu zaidi. *** Na hayo ndiyo tutayafanya Mungu akitupa kibali. Baada ya watu kuiacha njia ya Kristo, je unaweza kuwafanya wabadilike tena katika maisha yao? Ninazungumzia wale watu ambao mwanzo walijifunza kweli, wakapokea karama za Mungu, na kushiriki katika Roho Mtakatifu. Walibarikiwa kusikia ujumbe mzuri wa Mungu na kuziona nguvu kuu za ulimwengu wake mpya. Lakini baadaye waliziacha zote, na siyo rahisi kuwafanya wabadilike tena. Ndiyo sababu wale watu wanaomwacha Kristo wanamsulibisha msalabani kwa mara nyingine, wakimwaibisha yeye mbele ya kila mtu. *** *** Watu wengine wako kama ardhi inayopata mvua nyingi na kuzaa mazao mazuri kwa wale wanaoilima. Aina hiyo ya ardhi inazo baraka za Mungu. Lakini watu wengine wako kama ardhi ambayo huzalisha miiba na magugu tu. Haifai na iko katika hatari ya kulaaniwa na Mungu. Itateketezwa kwa moto. Rafiki zangu, sisemi haya kwa sababu nafikiri kuwa yanawatokea ninyi. Kwa hakika tunatarajia kuwa mtafanya vizuri zaidi; kwamba mtayafanya mambo mema yatakayotokea katika wokovu wenu. Mungu ni wa haki, na ataikumbuka kila kazi mliyoifanya. Atakumbuka kuwa mliuonesha upendo wenu kwake kwa kuwasaidia watu wake na kwamba mnaendelea kuwasaidia. Tunamtaka kila mmoja wenu awe radhi na mwenye shauku ya kuuonyesha upendo kama huo katika maisha yenu yote. Ndipo mtakapokuwa na uhakika wa kupata kile mnachokitumaini. Hatupendi muwe wavivu. Tunapenda muwe kama wale, kwa sababu ya imani yao na uvumilivu, watapokea kile Mungu alichoahidi. Mungu aliweka ahadi kwa Ibrahimu. Na hayuko yeyote aliye mkuu kuliko Mungu, hivyo akaweka ahadi yenye kiapo kwa jina lake mwenyewe; kiapo ambacho atatimiza alichoahidi. Alisema, “Hakika nitakubariki. Nitakupa wewe wazaliwa wengi.” Ibrahimu akangoja kwa uvumilivu hili litimie, na baadaye akapokea kile Mungu alichoahidi. Mara nyingi watu hutumia jina la mtu aliye mkuu zaidi yao ili kuweka ahadi yenye kiapo. Kiapo huthibitisha kwamba walichokisema ni kweli, na hakuna haja ya kubishana juu ya hilo. Mungu alitaka kuthibitisha kuwa ahadi yake ilikuwa kweli. Alitaka kuthibitisha hili kwa wale ambao wataipokea ahadi. Aliwataka waelewe kwa uwazi kwamba makusudi yake kamwe hayabadiliki. Hivyo Mungu akisema kitu fulani kingetokea, na akathibitisha aliyosema kwa kuongezea kiapo. Mambo haya mawili hayawezi kubadilika: Mungu hawezi kusema uongo anaposema kitu, na hawezi kudanganya anapoweka kiapo. Hivyo mambo yote hayo ni ya msaada mkubwa kutusaidia sisi tuliomjia Mungu kwa ajili ya usalama. Yanatuhimiza kuling'ang'ania tumaini lililo letu. Tumaini hili tulilonalo ni kama nanga kwetu. Ni imara na la uhakika na hutulinda salama. Huenda hadi nyuma ya pazia katika mahali patakatifu zaidi kwenye hekalu la kimbingu la Mungu. Tayari Yesu amekwisha kuingia hapo na kuifungua njia kwa ajili yetu. Amefanyika kuhani mkuu milele, kama alivyokuwa Melkizedeki. Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu. Alikutana na Ibrahimu wakati Ibrahimu alipokuwa akirudi baada ya kuwashinda wafalme. Siku hiyo Melkizedeki alimbariki Ibrahimu. Kisha Ibrahimu akampa sehemu ya kumi ya kila kitu alichokuwa nacho. Jina Melkizedeki, mfalme wa Salemu, lilikuwa na maana mbili. Kwanza, Melkizedeki inamaanisha “mfalme wa haki.” Na “mfalme wa Salemu” inamaanisha “mfalme wa amani.” Hakuna ajuaye baba na mama yake walikuwa ni kina nani au walitokea wapi. Na hakuna ajuaye alizaliwa lini au alikufa lini. Melkizedeki ni kama Mwana wa Mungu kwa vile siku zote atakuwa kuhani. Unaweza kuona kuwa Melkizedeki alikuwa mkuu sana. Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa yeye sehemu ya kumi ya kila alichoshinda kule vitani. Sasa sheria inasema kwamba wale wa ukoo wa Lawi waliokuja kuwa makuhani wanastahili kupata sehemu ya kumi kutoka kwa watu wao, hata kama wao na watu wao ni wa familia ya Ibrahimu. Melkizedeki wala hakutoka katika kabila la Lawi, lakini Ibrahimu akampa sehemu ya kumi ya alivyokuwa navyo. Na Melkizedeki akambariki Ibrahimu yule aliyekuwa na ahadi za Mungu. Na kila mtu anajua kwamba mtu aliye wa muhimu zaidi humbariki mtu yule ambaye ana umuhimu mdogo. Makuhani hawa hupata sehemu ya kumi, lakini wao ni binadamu tu wanaoishi kisha hufa. Lakini Melkizedeki, aliyepata sehemu ya kumi kutoka kwa Ibrahimu, anaendelea kuishi, kama Maandiko yanavyosema. Sasa wale wa kutoka ukoo wa Lawi ndiyo wanaopata sehemu ya kumi kutoka kwa watu. Lakini tunaweza kusema kuwa Ibrahimu alipompa Melkizedeki sehemu ya kumi, kisha Lawi naye akatoa. Lawi alikuwa bado hajazaliwa, lakini alikuwepo katika baba yake Ibrahimu wakati Melkizedeki alipokutana naye. Watu walipewa sheria chini ya mfumo wa makuhani waliotoka katika ukoo wa Lawi. Lakini hayupo awezaye kufanywa mkamilifu kiroho kwa njia ya mfumo wa makuhani. Hivyo lilikuwepo hitaji la kuhani mwingine kuja. Namaanisha kama Melkizedeki, siyo Haruni. Na anapokuja kuhani wa aina nyingine, basi sheria pia inabidi ibadilishwe. Tunazungumza juu ya Bwana Yesu, aliyetoka katika kabila lingine. Hakuwepo yeyote kutoka katika kabila hilo kamwe aliyeweza kutumika kama kuhani madhabahuni. Ni dhahiri kwamba Bwana Yesu alitoka katika kabila la Yuda. Na Musa hakusema chochote kuhusu makuhani waliyetokana na kabila hilo. *** Na mambo haya yalizidi kuwa wazi zaidi tunapomwona kuhani mwingine aliye kama Melkizedeki. Alifanywa kuhani, lakini siyo kwa sababu alikamilisha mahitaji ya kuzaliwa katika familia sahihi. Alifanyika kuhani kwa nguvu ya uhai ambayo haitakwisha. Hivi ndivyo Maandiko yanavyosema kumhusu yeye: “Wewe ni kuhani milele, kama alivyokuwa Melkizedeki.” Hivyo mfumo wa sheria za zamani zilizowekwa sasa zinaisha kwa sababu zilikuwa dhaifu na hazikuweza kutusaidia. Sheria ya Musa haikuweza kukamilisha kitu chochote. Lakini sasa tumaini bora zaidi limeletwa kwetu. Na kwa tumaini hilo tunaweza kumkaribia Mungu. Vile vile, ni muhimu kwamba Mungu aliweka ahadi kwa kiapo alipomfanya Yesu kuwa kuhani mkuu. Watu hawa wengine walipofanyika makuhani, hapakuwepo kiapo. Lakini Yesu akafanyika kuhani kwa kiapo cha Mungu. Mungu alimwambia: “Bwana anaweka ahadi kwa kiapo naye hatabadili mawazo yake: ‘Wewe ni kuhani milele.’” Hivyo hii inamaanisha kwamba Yesu ni uhakika wa agano zuri zaidi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wake. Pia, mmoja wa hawa makuhani wengine alipofariki, asingeendelea kuwa kuhani. Hivyo walikuwepo makuhani wengi wa jinsi hii. Lakini Yesu anaishi milele. Hatakoma kufanya kazi kama kuhani. Hivyo anaweza kuwaokoa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake. Yesu anaweza kufanya hivi milele, kwa sababu anaishi siku zote na yuko tayari kuwasaidia watu wanapomjia Mungu. Hivyo Yesu ni aina ya kuhani mkuu tunayemhitaji. Yeye ni mkamilifu. Hana dhambi ndani yake. Hana kasoro na havutwi na watenda dhambi. Naye amepandishwa juu ya mbingu. Hayuko sawa na hawa makuhani wengine. Walitakiwa kutoa sadaka kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zao wenyewe, na kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Lakini Yesu hahitaji kufanya hivyo. Alitoa sadaka moja tu kwa ajili ya nyakati zote. Alijitoa mwenyewe. Sheria huchagua makuhani wakuu ambao ni watu na wanao udhaifu ule ule ambao watu wote wanao. Lakini baada ya sheria, Mungu alisema kiapo ambacho kilimfanya Mwana awe kuhani mkuu. Na Mwana huyo, aliyekamilishwa kwa njia ya mateso, atatumika kama kuhani mkuu milele yote. Hii ndiyo hoja tunayosema: Tunaye kuhani mkuu wa jinsi hiyo, anayeketi upande wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu Mkuu mbinguni. Kuhani wetu mkuu anahudumia katika Patakatifu pa Patakatifu. Anahudumia katika mahali pa hakika kwa ibada palipotengenezwa na Bwana, siyo na mtu yeyote duniani. Kila kuhani mkuu anayo kazi ya kutoa sadaka na sadaka kwa Mungu. Hivyo kuhani wetu mkuu pia anahitajika kutoa kitu kwa Mungu. Kama kuhani wetu mkuu angekuwa anaishi duniani, asingekuwa kuhani. Nasema hivi kwa sababu tayari hapa wapo makuhani ambao wanafuata sheria kwa kutoa sadaka kwa Mungu. Kazi ambayo makuhani hawa wanafanya hakika ni nakala tu na kivuli cha yaliyoko mbinguni. Ndiyo sababu Mungu alimwonya Musa alipokuwa amejiandaa kujenga Hema Takatifu: “Uwe na uhakika kufanya kila kitu sawasawa na kielelezo nilichokuonesha kule mlimani.” Lakini kazi ambayo tayari imetolewa kwa Yesu ni kuu zaidi ya kazi iliyotolewa na makuhani hao. Kwa jinsi hiyo hiyo, agano jipya ambalo Yesu alilileta kutoka kwa Mungu kuja kwa watu wake ni kuu zaidi kuliko lile la zamani. Na agano jipya limeelemea katika ahadi bora zaidi. Kama kusingekuwa na makosa katika agano la kwanza, kisha kusingekuwa na haja ya agano la pili. Lakini Mungu aligundua kitu kilichokuwa na kasoro kwa watu, akasema: “Wakati unakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na watu wa Israeli na watu wa Yuda. Halitakuwa sawa na agano lililotengenezwa na baba zao. Hilo ni agano nililowapa nilipowachukua kwa mkono na kuwatoa Misri. Hawakuendelea kufuata agano nililowekeana nao, na nikageuka mbali nao, asema Bwana. Hili ni agano jipya nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana: Nitaziweka sheria zangu katika fahamu zao, na nitaandika sheria zangu katika mioyo yao. Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Hakuna tena atakayemfundisha jirani yake au familia yake kumjua Bwana. Watu wote, wakuu zaidi na wasio na umuhimu kabisa, watanijua. Na nitawasamehe makosa waliyotenda, na sitazikumbuka dhambi zao.” Mungu aliliita hili ni agano jipya, hivyo amelifanya agano la kwanza kuwa la zamani. Na chochote kilicho cha zamani na kisichokuwa na matumizi kiko tayari kutoweka. Patano la kwanza lilikuwa na kanuni kwa ajili ya kuabudu na mahali pa kuabudia hapa duniani. Mahali hapa palikuwa ni ndani ya hema. Eneo la kwanza ndani ya hema liliitwa Patakatifu. Katika Patakatifu kulikuwepo taa na meza iliyokuwa na mikate maalumu iliyotolewa kwa Mungu. Nyuma ya pazia la pili kilikuwepo chumba kilichoitwa Patakatifu pa Patakatifu. Katika Patakatifu pa Patakatifu kulikuwepo madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kuchoma uvumba. Pia lilikuwepo Sanduku la Agano. Sanduku lilifunikwa kwa dhahabu. Ndani ya hilo Sanduku kulikuwemo birika la mana na fimbo ya Haruni; fimbo ambayo iliwahi kuchipusha matawi. Vilevile ndani ya Sanduku yalikuwemo mawe bapa yaliyoandikwa Amri Kumi za agano la kale kwao. Juu ya Sanduku walikuwepo viumbe wenye mbawa walioonesha utukufu wa Mungu. Viumbe hawa wenye mbawa walikuwa juu ya sehemu ya rehema. Lakini hatuwezi kusema chochote kuhusu hili hivi sasa. Kila kitu ndani ya hema kilikuwa kimewekwa tayari kwa namna nilivyoeleza. Kisha makuhani waliingia ndani ya chumba cha kwanza kila siku kutekeleza shughuli zao za ibada. Lakini ni kuhani mkuu tu aliweza kuingia kwenye chumba cha pili, na aliingia mara moja tu kwa mwaka. Pia, asingeweza kuingia ndani ya chumba hicho bila kuchukua damu pamoja naye. Aliitoa damu hiyo kwa Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi walizotenda watu bila kujua kwamba walikuwa wanatenda dhambi. Roho Mtakatifu hutumia vyumba hivi viwili tofauti kutufundisha kwamba njia ya kuelekea Patakatifu pa Patakatifu haikuwa wazi wakati chumba cha kwanza kilipokuwepo. Huu ni mfano kwetu leo. Inaonyesha sadaka na sadaka ambazo makuhani walizitoa kwa Mungu haziwezi kufanya dhamiri za wanaoabudu ziwe safi kabisa. Sadaka na sadaka hizi ni kwa ajili tu ya vyakula na vinywaji na aina maalumu ya kuoga. Ni sheria kuhusu mwili tu. Mungu alizitoa kwa watu wake wazifuate hadi wakati wa njia yake mpya. Lakini Kristo tayari amekuja awe kuhani mkuu. Yeye ni kuhani mkuu wa mambo mema tuliyonayo sasa. Lakini Kristo hatumiki ndani ya eneo kama hema ambalo makuhani wale walitumika ndani yake. Anatumika katika eneo bora zaidi. Tofauti na hema lile, hili ni kamilifu. Halikutengenezwa hapa duniani. Siyo la ulimwengu huu. Kristo aliingia Patakatifu Zaidi mara moja tu; hii ilitosha kwa nyakati zote. Aliingia Patakatifu Zaidi kwa kutumia damu yake mwenyewe, siyo damu ya mbuzi au ya ng'ombe wadogo. Aliingia hapo na kutuweka huru milele kutoka katika dhambi. Damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ng'ombe zilinyunyizwa juu ya wale ambao hawakuwa safi vya kutosha tena kuweza kuingia katika eneo la kuabudia. Damu na majivu viliwafanya wawe safi tena, lakini katika miili yao tu. Hivyo hakika sadaka ya damu ya Kristo inaweza kufanya mambo bora zaidi. Kristo alijitoa mwenyewe kupitia Roho wa milele kama sadaka kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa kabisa sisi kutoka katika maovu tuliyotenda. Itatupa sisi dhamiri safi ili tuweze kumwabudu Mungu aliye hai. Hivyo Kristo huwaletea watu wake agano jipya kutoka kwa Mungu. Huleta agano hili ili wale walioteuliwa na Mungu waweze kuzipata baraka ambazo Mungu aliwaahidi, baraka zinazodumu milele. Hili laweza kutokea tu kwa sababu Kristo alikufa ili awaweke huru watu kutokana na dhambi zilizotendwa dhidi ya amri za agano la kwanza. Mtu anapofariki na akaacha usia, ni lazima uwepo uthibitisho kwamba yule aliyeandika usia amefariki. Usia haumaanishi chochote wakati aliyeuandika bado yuko hai. Unaweza kutumika mara tu baada ya kifo cha mtu huyo. Ndiyo sababu ili kuthibitisha kifo damu ilihitajika ili kuanza agano la kwanza baina ya Mungu na watu wake. Kwanza, Musa aliwaeleza watu kila agizo katika sheria. Kisha akachukua damu ya ndama dume na kuichanganya na maji. Alitumia sufu nyekundu na tawi la hisopo kunyunyiza damu na maji katika kitabu cha sheria na kwa watu. Kisha akasema, “Hii ni damu inayoweka agano liwe zuri agano ambalo Mungu aliwaagiza mlifuate.” Kwa jinsi hiyo hiyo, Musa alinyunyiza damu katika Hema Takatifu. Aliinyunyiza damu juu ya kila kitu kilichotumika katika ibada. Sheria inasema kwamba karibu kila kitu kinapaswa kutakaswa kwa damu. Dhambi haziwezi kusamehewa bila sadaka ya damu. Mambo haya ni nakala ya mambo halisi yaliyoko mbinguni. Nakala hizi zinapaswa kutakaswa kwa sadaka ya wanyama. Lakini mambo halisi yaliyoko mbinguni yanapaswa kuwa na sadaka zilizo bora zaidi. Kristo alienda katika Patakatifu pa Patakatifu. Lakini hapakuwa mahali palipotengenezwa na mwanadamu, ambapo ni nakala tu ya ile iliyo halisi. Alienda katika mbingu, na yuko huko sasa mbele za Mungu ili atusaidie sisi. Kuhani mkuu huingia katika Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kila mwaka. Huchukua pamoja naye damu ya sadaka. Lakini hatoi damu yake kama alivyofanya Kristo. Kristo alienda mbinguni, lakini siyo kujitoa mwenyewe mara nyingi kama ambavyo kuhani mkuu hutoa damu tena na tena. Kama Kristo alijitoa mwenyewe mara nyingi, basi angehitaji kuteseka mara nyingi tangu wakati dunia ilipoumbwa. Lakini alikuja kujitoa mwenyewe mara moja tu. Na mara hiyo moja inatosha kwa nyakati zote. Alikuja katika wakati ambao ulimwengu unakaribia mwisho. Alikuja kuchukua dhambi zote kwa kujitoa mwenyewe kama sadaka. Kila mtu atakufa mara moja tu. Baada ya hapo ni kuhukumiwa. Hivyo Kristo alitolewa kama sadaka mara moja kuchukua dhambi za watu wengi. Na atakuja mara ya pili, lakini siyo kujitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi. Atakuja mara ya pili kuleta wokovu kwa wale wanaomngojea. Sheria ya Musa ilitupa sisi picha tu isiyo wazi sana ya mambo yaliyokuwa yanakuja baadaye. Sheria siyo picha kamili ya mambo halisi. Sheria huwaambia watu kutoa sadaka zile zile kila mwaka. Wale wanaokuja kumwabudu Mungu wanaendelea kutoa sadaka. Lakini sheria haiwezi kamwe kuwakamilisha wao. Kama sheria ingeweza kuwakamilisha watu, sadaka hizi zingekuwa zimekoma. Tayari wao wangekuwa safi kutoka katika dhambi, na bado wasingehukumiwa moyoni mwao. Lakini hayo siyo yanayotokea. Dhabihu zao zinawafanya wazikumbuke dhambi zao kila mwaka, kwa sababu haiwezekani kwa damu ya fahali na mbuzi kuondoa dhambi. Hivyo baada ya Kristo kuja ulimwenguni alisema: “Huhitaji sadaka na sadaka, lakini umeandaa mwili kwa ajili yangu. Hukuridhishwa na sadaka za kuteketezwa na sadaka kuondoa dhambi. Kisha nikasema, ‘Nipo hapa, Mungu. Imeandikwa juu yangu katika kitabu cha sheria. Nimekuja kufanya yale unayopenda.’” Kwanza Kristo alisema, “Wewe hufurahishwi na sadaka na sadaka. Hukuridhishwa na sadaka za kuteketezwa na sadaka ili kuondoa dhambi.” (Hizi ndizo sadaka zote ambavyo sheria inaagiza.) Kisha akasema, “Niko hapa, Mungu. Nimekuja kufanya yale unayopenda.” Hivyo Mungu akafikisha mwisho wa mfumo wa zamani wa utoaji sadaka na akaanzisha njia mpya. Yesu Kristo alifanya mambo ambayo Mungu alimtaka ayafanye. Na kwa sababu ya hilo, tunatakaswa kwa njia ya sadaka ya mwili wa Kristo. Kristo aliitoa sadaka hiyo mara moja, inayotosha kwa nyakati zote. Kila siku makuhani husimama na kutekeleza shughuli zao za kidini. Tena na tena hutoa sadaka zilezile, ambazo kamwe haziwezi kuondoa dhambi. Lakini Kristo alitoa sadaka moja tu kwa ajili ya dhambi, na sadaka hiyo ni nzuri kwa nyakati zote. Kisha akakaa mkono wa kuume wa Mungu. Na sasa Kristo anawasubiria hapo adui zake wawekwe chini ya mamlaka yake. Kwa sadaka moja Kristo akawakamilisha watu wake milele. Ndio wale wanaotakaswa. Roho Mtakatifu pia anatuambia juu ya hili. Kwanza anasema: “Hili ndilo agano nitakaloweka na watu wangu baadaye, asema Bwana. Nitaziweka sheria zangu ndani ya mioyo yao. Nitaziandika sheria zangu katika fahamu zao.” Kisha anasema, “Nitazisahau dhambi zao na nisikumbuke kamwe uovu walioutenda.” Na baada ya kila kitu kusamehewa, hakuna tena haja ya sadaka ili kuziondoa dhambi. Hivyo ndugu na dada, tuko huru kabisa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu. Tunaweza kufanya hivi bila hofu kwa sababu ya sadaka ya damu ya Yesu. Tunaingia kwa njia mpya ambayo Yesu alitufungulia. Ni njia iliyo hai inayotuelekeza kupitia pazia; yaani mwili wa Yesu. Na tunaye kuhani mkuu zaidi anayeisimamia nyumba ya Mungu. Ikiwa imenyunyiziwa kwa damu ya Kristo, mioyo yetu imewekwa huru kutokana na dhamiri yenye hukumu, na miili yetu imeoshwa kwa maji safi. Hivyo mkaribieni Mungu kwa moyo safi, mkijaa ujasiri kwa sababu ya imani katika Kristo. Tunapaswa kuling'ang'ania tumaini tulilonalo, bila kusitasita kuwaeleza watu juu yake. Tunaweza kumwamini Mungu kuwa atatimiza aliyoahidi. Tunahitaji kumfikiria kila mtu kuona jinsi tunavyoweza kuhamasishana kuonesha upendo na kazi njema. Tusiache kukutana pamoja, kama wanavyofanya wengine. Hapana, tunahitaji kuendelea kuhimizana wenyewe. Hili linazidi kuwa muhimu zaidi na zaidi kadri mnavyoona ile Siku inakaribia. Kama tutaamua kuendelea kutenda dhambi baada ya kujifunza ukweli, ndipo hakutakuwa sadaka nyingine itakayoondoa dhambi. Tukiendelea kutenda dhambi, kitakachokuwa kimebaki kwetu ni wakati wa kutisha wa kuingoja hukumu na moto wa hasira utakaowaangamiza wale wanaoishi kinyume na Mungu. Yeyote aliyekataa kuitii Sheria ya Musa alipatikana ana hatia kutokana na ushuhuda uliotolewa na mashahidi wawili au watatu. Watu wa jinsi hiyo hawakusamehewa. Waliuawa. Hivyo fikiri jinsi watu watakavyostahili kuhukumiwa zaidi ambao wanaonesha kumchukia mwana wa Mungu; watu wanaoonesha kuwa hawana heshima kwa sadaka ya damu iliyoanzisha agano jipya na mara moja ikawatakasa au wale wanaomkashifu Roho wa neema ya Mungu. Tunajua kuwa Mungu alisema, “Nitawaadhibu watu kwa ajili ya makosa wanayofanya”; nitawalipa tu Pia alisema, “BWANA atawahukumu watu wake.” Ni jambo la kutiisha kukutana na hukumu kutoka kwa Mungu aliye hai. Zikumbukeni siku za kwanza mlipojifunza kweli. Mlikuwa na mashindano magumu pamoja na mateso mengi, lakini mkaendelea kuwa imara. Mara zingine watu waliwasemea mambo ya chuki na kuwatesa hadharani. Na nyakati zingine mliwasaidia wengine waliokuwa wakitendewa vivyo hivyo. Ndiyo, mliwasaidia magerezani na kushiriki katika mateso yao. Na bado mlikuwa na furaha wakati kila kitu mlichokimiliki kilipochukuliwa kutoka kwenu. Mkaendelea kufurahi, kwa sababu mlijua kwamba mnacho kitu kilicho bora zaidi; kitu kitakachoendelea milele. Hivyo msipoteze ujasiri mliokuwa nao zamani. Ujasiri wenu utalipwa sana. Mnahitajika kuwa na subira. Baada ya kufanya yale anayotaka Mungu, mtapata aliyowaahidi. “Karibu sana sasa, yeye ajaye atakuja wala hatachelewa. Mtu aliye sahihi mbele zangu ataishi akiniamini mimi. Lakini sitafurahishwa na yule anayegeuka nyuma kwa ajili ya woga.” Lakini sisi siyo wale wanaogeuka nyuma na kuangamia. Hapana, sisi ni watu walio na imani na tunaokolewa. Imani inaleta uthabiti wa mambo tunayoyatarajia. Ni uthibitisho wa yale tusiyoweza kuyaona. Mungu alifurahishwa na watu walioishi muda mrefu uliopita kwa sababu walikuwa na imani ya namna hii. Imani hutusaidia sisi kufahamu kwamba Mungu aliumba ulimwengu wote kwa amri yake. Hii inamaanisha kwamba vitu tunavyoviona viliumbwa kwa kitu kisichoonekana. Kaini na Habili wote walitoa sadaka kwa Mungu. Lakini Habili alitoa sadaka bora zaidi kwa Mungu kwa sababu alikuwa na imani. Mungu akasema alifurahishwa na kile alichotoa Habili. Na hivyo Mungu akamwita kuwa mtu mwema kwa sababu alikuwa na imani. Habili akafariki, lakini kupitia imani yake bado anazungumza. Henoko alitwaliwa kutoka duniani, hivyo kamwe yeye hajafariki. Maandiko yanatueleza kwamba kabla ya kuchukuliwa, alikuwa mtu aliyempendeza Mungu. Baadaye, hayupo yeyote aliyejua kule alikokuwa, kwa sababu Mungu alimchukua Henoko ili awe pamoja naye. Haya yote yakatokea kwa vile alikuwa na imani. Bila kuwa na imani hakuna anayeweza kumfurahisha Mungu. Yeyote anayemjia Mungu anatakiwa kuamini kwamba yeye ni hakika na kwamba anawalipa wale ambao kwa uaminifu wanajitahidi kumtafuta. Nuhu alionywa na Mungu juu ya mambo ambayo hakuwa ameyaona bado. Lakini alikuwa na imani na heshima kwa Mungu, hivyo akaijenga meli kubwa ili kuiokoa familia yake. Kwa imani yake, Nuhu alionesha kwamba ulimwengu ulikuwa umekosea. Na akawa ni mmoja wa wale waliohesabiwa haki na Mungu kwa njia ya imani. Mungu alimwita Ibrahimu kusafiri kwenda sehemu ingine aliyoahidi kumpa. Ibrahimu hakujua hiyo sehemu ingine ilikuwa wapi. Lakini alimtii Mungu na akaanza kusafiri kwa sababu alikuwa na imani. Ibrahimu akaishi katika nchi ambayo Mungu aliahidi kumpa. Akaishi humo kama mgeni tu asiyekuwa mwenyeji. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. Akaishi katika mahema pamoja na Isaka na Yakobo, ambao pia walipokea ahadi ile ile kutoka kwa Mungu. Ibrahimu alikuwa anaungoja mji ambao ulikuwa na misingi halisi. Alikuwa anaungoja mji ulibuniwa na kujengwa na Mungu. Sara hakuwa na uwezo wa kupata watoto, na Ibrahimu alikuwa amezeeka sana. Lakini alikuwa anamwamini Mungu, akimwamini kuwa anaweza kutenda yale aliyoahidi. Hivyo Mungu akawawezesha kupata watoto. Ibrahimu alikuwa amezeeka sana karibu ya kufa. Lakini kupitia kwa mtu huyo mmoja vikaja vizazi vingi kama zilivyo nyota za angani. Hivyo watu wengi wakaja kutoka kwake wakiwa kama punje za mchanga katika ufukwe wa bahari. Watu hawa wote mashuhuri wakaendelea kuishi kwa imani hadi walipofariki. Hawakuwa wamepata mambo ambayo Mungu aliwaahidi watu wake. Lakini walikuwa na furaha kuona tu kwamba ahadi hizi zilikuwa zinakuja kwa mbali siku zijazo. Waliukubali ukweli kwamba wao walikuwa kama wageni na wasafiri hapa duniani. Watu wanapolikubali jambo la namna hiyo, wanaonesha kuwa wanaingojea nchi itakayokuwa yao wenyewe. Kama wangekuwa wanaifikiria nchi walikotoka, wangekuwa wamerejea. Lakini walikuwa wanaingoja nchi iliyo bora zaidi, nchi ya mbinguni. Hivyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao. Naye amewaandalia mji. Mungu aliijaribu imani ya Ibrahimu. Mungu alimtaka amtoe Isaka kama sadaka. Ibrahimu akatii kwa sababu alikuwa na imani. Tayari alikuwa na ahadi kutoka kwa Mungu. Na Mungu tayari alikuwa amekwishamwambia, “Ni kupitia kwa Isaka kwamba vizazi vyako watakuja.” Lakini Ibrahimu alikuwa tayari kumtoa mwana wake wa pekee. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. *** Aliamini kwamba Mungu angeweza kuwafufua watu kutoka kifoni. Na hakika, Mungu alipomzuia Ibrahimu katika kumuua Isaka, ilikuwa ni kama vile alimpata tena kutoka kifoni. Isaka akayabariki maisha ya mbeleni ya Yakobo na Esau. Alifanya hivyo kwa sababu alikuwa na imani. Na Yakobo, pia kwa vile alikuwa na imani, alimbariki kila mmoja wa wana wa Yusufu. Alifanya haya wakati alipokuwa akifa, akaiegemea fimbo yake akimwabudu Mungu. Na Yusufu alipokuwa karibu amefariki, alizungumza kuhusu watu wa Israeli kuondoka Misri. Na aliwaambia yale waliyotakiwa kuufanyia mwili wake. Alifanya haya kwa sababu alikuwa na imani. Na mama na baba wa Musa wakaona kwamba alikuwa ni mtoto mzuri hivyo wakamficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Hili lilikuwa kinyume na agizo la mfalme. Lakini hawakuogopa kwa sababu walikuwa na imani. Musa akakua na akawa mwanaume. Akakataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kutokujifurahisha katika raha na dhambi zinazodumu kwa muda mfupi tu. Badala yake, akachagua kuteseka pamoja na watu wa Mungu. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. *** Alifikiri kuwa ni bora kuteseka kwa ajili ya Masihi kuliko kuwa na hazina zote za Misri. Alikuwa anaisubiri malipo ambayo Mungu angempa. Musa akaondoka Misri kwa sababu alikuwa na imani. Hakuiogopa hasira ya mfalme. Aliendelea kuwa jasiri kama vile angemwona Mungu ambaye hakuna mtu mwingine angeweza kumwona. Na kwa sababu alikuwa na imani, Musa akaandaa mlo wa Pasaka. Na akanyunyiza damu ya mwanakondoo katika miimo ya milango ya watu wake, ili kwamba malaika wa kifo asiwaue wazaliwa wao wa kwanza wa kiume. Na watu wa Mungu wote wakatembea kuvuka Bahari ya Shamu kama vile ilikuwa ni ardhi kavu. Waliweza kufanya hivi kwa sababu walikuwa na imani. Lakini wakati Wamisri walipojaribu kuwafuata, wote wakazama majini. Na kuta za Yeriko zilianguka kwa ajili ya imani ya watu wa Mungu. Walitembea kuuzunguka ukuta kwa siku saba, na kisha kuta zikaanguka. Na Rahabu, yule kahaba, aliwakaribisha wapelelezi wa Kiisraeli kama marafiki. Na kwa sababu ya imani yake, hakuuawa pamoja na wale waliokataa kutii. Je, nahitaji niwape mifano zaidi? Sina muda wa kutosha kuwaeleza kuhusu Gidioni, Baraki, Samsoni, Yefta, Daudi, Samweli na manabii. Wote walikuwa na imani kuu. Na kwa njia ya imani hiyo wakaziangusha falme. Wakafanya kilichokuwa sahihi, na Mungu akawasaidia katika njia alizoahidi. Kwa imani zao watu wengine waliifunga midomo ya simba. Na wengine waliweza kuizuia miali ya moto. Wengine wakaepuka katika kuuawa kwa upanga. Wengine waliokuwa dhaifu wakafanywa wenye nguvu. Wakawa na nguvu katika vita na kuyaangusha majeshi mengine. Walikuwepo wanawake waliowapoteza wapendwa wao lakini wakawapata tena walipofufuliwa kutoka wafu. Wengine waliteswa lakini wakakataa kuukubali uhuru wao. Walifanya hivi ili waweze kufufuliwa kutoka kifoni kuingia katika maisha bora zaidi. Wengine walichekwa na kupigwa. Wengine walifungwa na kutiwa magerezani. Waliuawa kwa mawe. Walikatwa vipande viwili. Waliuawa kwa panga. Mavazi pekee wengine wao waliyokuwa nayo yalikuwa ni ngozi za kondoo au za mbuzi. Walikuwa maskini, waliteswa, na kutendewa mabaya na wengine. Ulimwengu haukustahili kuwa na watu wakuu na waaminifu kama hawa. Hawa waliweza kuzunguka jangwani na milimani, wakiishi katika mapango na mashimo ardhini. Mungu alifurahishwa nao wote kwa sababu ya imani zao. Lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea ahadi ya Mungu. Mungu alikusudia kitu bora zaidi kwa ajili yetu. Alitaka kutukamilisha sisi. Hakika, pia alitaka watu hawa wakuu wakamilishwe, lakini siyo kabla ya sisi wote kuzifurahia baraka pamoja. Tunao hawa watu mashuhuri wakituzunguka kama mifano kwetu. Maisha yao yanatueleza imani ni nini. Hivyo, nasi pia, tunapaswa kufanya mashindano yaliyo mbele yetu na kamwe tusikate tamaa. Tunapaswa kuondoa katika maisha yetu kitu chochote kitakachotupunguzia mwendo pamoja na dhambi zinazotufanya tutoke kwenye mstari mara kwa mara. Hatupaswi kuacha kumwangalia Yesu. Yeye ndiye kiongozi wa imani yetu, na ndiye anayeikamilisha imani yetu. Aliteseka hadi kufa msalabani. Lakini aliikubali aibu ya msalaba kama kitu kisicho na maana kwa sababu ya furaha ambayo angeiona ikimngojea. Na sasa ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Mfikirie Yesu. Kwa uvumilivu alistahimili matusi ya hasira ya watenda dhambi waliokuwa wakiwapigia kelele. Mfikirie yeye ili usikate tamaa na kuacha kujaribu. Mnashindana na dhambi, lakini bado hamjamwaga damu hata kuutoa uhai wenu katika mashindano hayo. Ninyi ni watoto wa Mungu, naye huzungumza maneno ya faraja kwenu. Labda mmeyasahau maneno haya: “Mwanangu, wakati Mungu anapokurekebisha, zingatia na usiache kujaribu. Bwana humrekebisha kila anayempenda; humpa adhabu kila anayemkubali kama mwana wake.” Hivyo muyapokee mateso kama adhabu ya baba. Mungu hufanya mambo haya kwenu kama baba anavyowarekebisha watoto wake. Mnajua kuwa watoto wote hurekebishwa na baba zao. Hivyo, kama hukupata marekebisho ambayo kila mtoto anapaswa kuyapata, wewe siyo mtoto wa kweli na hakika wewe siyo wa Mungu. Sisi wote tulikuwa na baba wa hapa duniani walioturekebisha, na tuliwaheshimu. Ni muhimu zaidi basi kwamba tunapaswa kuyapokea marekebisho kutoka kwa Baba wa roho zetu. Tukifanya hivyo, tutakuwa na uzima. Baba zetu wa duniani waliturekebisha kwa muda mfupi katika njia waliyofikiri ilikuwa bora zaidi. Lakini Mungu huturekebisha sisi ili atusaidie tuweze kuwa watakatifu kama yeye. Hatufurahii marekebisho tunapokuwa tunayapata. Yanauma. Lakini baadaye, baada ya kujifunza somo kutokana na hayo, tutaifurahia amani itakayokuja kwa njia ya kufanya yaliyo sahihi. Mmekuwa dhaifu, hebu mjitie nguvu tena. Muishi katika njia iliyo sahihi ili muweze kuokolewa na udhaifu wenu hautawasababisha ninyi kupotea. Jitahidini kuishi kwa amani na kila mtu. Na mjitahidi kuyaweka mbali na dhambi maisha yenu. Yeyote ambaye maisha yake siyo matakatifu hawezi kumwona Bwana. Muwe makini ili mtu asije akakosa kuipata neema ya Mungu. Muwe makini ili asiwepo atakayepoteza imani yake na kuwa kama gugu chungu linalomea miongoni mwenu. Mtu wa jinsi hiyo anaweza kuharibu kundi lenu lote. Muwe makini ili asiwepo yeyote atakayefanya dhambi ya uzinzi au kushindwa kumheshimu Mungu moyoni kama alivyofanya Esau. Kama kijana mkubwa katika nyumba ya babaye, Esau angerithi sehemu kubwa ya vitu kutoka kwa baba yake. Lakini akauza kila kitu kwa mlo mmoja tu. Mnakumbuka kwamba baada ya Esau kufanya hivi, akataka kupata baraka za baba yake. Akaitamani sana baraka ile kiasi kwamba akalia. Lakini baba yake akakataa kumpa baraka hiyo, kwa sababu Esau hakupata njia ya kubadili yale aliyotenda. Ninyi ni watu wa Mungu, kama watu wa Israeli walipofika katika Mlima Sinai. Lakini hamjaufikia mlima halisi wa kuweza kushikwa. Mlima huo haupo kama ule waliouona, uliokuwa ukiwaka moto na kufunikwa na giza, utusitusi na dhoruba. Haipo sauti ya tarumbeta au sauti iliyoyasema maneno kama hayo waliyoyasikia. Walipoisikia sauti, wakasihi kamwe wasisikie neno lingine. Hawakutaka kusikia amri: “Kama chochote, hata mnyama, akigusa mlima, lazima kiuawe kwa kupigwa mawe.” Kile walichoona kilikuwa cha kutisha kiasi kwamba Musa akasema, “Natetemeka kwa hofu.” Lakini mmeufikia Mlima Sayuni, kwenye mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni. Mmefika mahali ambapo maelfu wa malaika wamekusanyika kusherehekea. Mmefika katika kusanyiko la watoto wazaliwa wa kwanza wa Mungu. Majina yao yameandikwa mbinguni. Mmemfikia Mungu, hakimu wa watu wote. Na mmefika kwenye roho za watu wema ambao wamekamilishwa. Mmemfikia Yesu; yeye aliyelileta kutoka kwa Mungu agano jipya kwenda kwa watu wake. Mmefika kwenye damu iliyonyunyizwa ambayo inasema habari za mema zaidi kuliko damu ya Habili. Muwe makini na msijaribu kupuuza kusikiliza Mungu anaposema. Watu wale walipuuza kumsikiliza yeye alipowaonya hapa duniani. Nao hawakuponyoka. Sasa Mungu anasema kutoka mbinguni. Hivyo sasa itakuwa vibaya zaidi kwa wale watakaopuuza kumsikiliza yeye. Alipozungumza pale mwanzoni, sauti yake iliitetemesha dunia. Lakini sasa ameahidi, “Kwa mara nyingine tena nitaitetemesha dunia, lakini pia nitazitetemesha mbingu.” Maneno “Kwa mara nyingine” yanatuonyesha kwa uwazi kwamba kila kitu kilichoumbwa kitaangamizwa; yaani, vitu vinavyoweza kutetemeshwa. Na ni kile tu kisichoweza kutetemeshwa kitakachobaki. Hivyo tunahitajika kuwa na shukrani kwa sababu tunao ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa. Na kwa sababu sisi ni watu wa shukrani, tunahitajika kumwabudu Mungu kwa njia itakayompendeza yeye. Tunahitajika kufanya hivi kwa heshima na hofu, kwa sababu “Mungu wetu yuko kama moto unaoweza kutuangamiza sisi.” Endeleeni kupendana ninyi kwa ninyi kama kaka na dada katika Kristo. Mkikumbuka kuwasaidia watu kwa kuwakaribisha majumbani mwenu. Watu wengine wamefanya hivyo na wakawa wamewasaidia malaika pasipo wao kujua. Msiwasahau wale walioko magerezani. Wakumbukeni kama vile mko magerezani pamoja nao. Na msiwasahau wale wanaoteseka. Wakumbukeni kama vile mnateseka pamoja nao. Ndoa iheshimiwe na kila mmoja. Na kila ndoa itunzwe kwa usafi kati ya mume na mke. Mungu atawahukumu kuwa na hatia wale wanaofanya uzinzi na uasherati. Yatunzeni maisha yenu yawe huru kutokana na kupenda fedha. Na mridhike na kile mlichonacho. Mungu amesema: “Sitakuacha kamwe; Sitakukimbia kamwe.” Hivyo tunaweza kuwa na uhakika na kusema: “Bwana ndiye msaidizi wangu; Sitaogopa. Watu hawawezi kunifanya chochote.” Wakumbukeni viongozi wenu. Waliwafundisha ujumbe wa Mungu. Kumbukeni jinsi walivyoishi na walivyokufa, na muiige imani yao. Yesu Kristo ni yule yule jana, leo na hata milele. Msiruhusu aina yoyote ya mafundisho mageni yawaongoze hadi katika njia isiyo sahihi. Itegemeeni neema ya Mungu pekee kwa ajili ya nguvu za kiroho, siyo katika sheria kuhusu vyakula. Kuzitii sheria hizi hakumsaidii yeyote. Tunayo sadaka. Na wale makuhani waliotumika ndani ya Hema Takatifu hawawezi kula sadaka tuliyo nayo. Kuhani mkuu hubeba damu za wanyama hadi Patakatifu pa Patakatifu na hutoa damu hiyo kwa ajili ya dhambi. Lakini miili ya wanyama hao huchomwa nje ya kambi. Hivyo Yesu naye alitesekea nje ya mji. Alikufa ili awatakase watu wake kwa damu yake mwenyewe. Hivyo tumwendee Yesu nje ya kambi na kuikubali aibu hiyo hiyo aliyoipata yeye. Hatuna mji unaodumu milele hapa duniani. Lakini tunaungoja mji tutakaoupata hapo baadaye. Hivyo kwa njia ya Yesu hatupaswi kuacha kumtolea Mungu sadaka zetu. Dhabihu hizo ni sifa zetu, zinazotoka katika vinywa vyetu vinavyolisema jina lake. Na msisahau kutenda mema na kushirikishana na wengine mlivyo navyo, kwa sababu sadaka kama hizi zinamfurahisha sana Mungu. Muwatii viongozi wenu. Muwe tayari kufanya yale wanayowaambia. Wanawajibika katika maisha yenu ya kiroho, hivyo nyakati zote wanaangalia jinsi ya kuwalinda ninyi. Muwatii ili kazi yao iwafurahishe wao, siyo kupata majonzi. Haitawasaidia ninyi mnapowasababishia matatizo. Endeleeni kutuombea. Tunajisikia tuko sahihi katika tunayoyafanya, kwa sababu nyakati zote tunajitahidi kadri tuwezavyo. Na nawasihi muombe ili Mungu anirudishe tena kwenu mapema. Nalitamani sana hili kuliko kitu chochote. Ninawaombea Mungu wa amani awape ninyi mambo mazuri mnayohitaji ili muweze kufanya anayoyapenda. Mungu ndiye aliyemfufua Bwana Yesu kutoka katika kifo, Mchungaji Mkuu wa kondoo wake. Alimfufua kwa sababu Yesu aliitoa sadaka ya damu yake ili kulianza agano jipya lisilo na mwisho. Namwomba Mungu atuwezeshe kwa njia ya Yesu Kristo kufanya mambo yanayompendeza yeye. Utukufu ni wake milele. Amina. *** Ndugu na dada zangu, nawasihi msikilize kwa uvumilivu katika yale niliyoyasema. Niliandika barua hii ili kuwatia moyo. Na siyo ndefu sana. Nawataka mjue kwamba ndugu yetu Timotheo ametoka gerezani. Akija kwangu mapema, sote tutakuja kuwaona ninyi. Fikisheni salama zangu kwa viongozi wote na kwa watu wote wa Mungu. Wote walioko Italia wanawasalimuni. Naomba neema ya Mungu iwe nanyi nyote. Kutoka kwa Yakobo mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo. Kwa makabila Kumi na Mawili ya watu wa Mungu yaliyotawanyika kote ulimwenguni: Salamu! Kaka na dada zangu, jueni kuwa mtakutana na adha za kila aina. Lakini hilo liwape ninyi sababu ya kuwa na furaha zaidi. Kwa sababu mnajua kuwa imani yenu inapojaribiwa ndipo mnapojifunza kuwa wavumilivu. Na uvumilivu unapaswa kukamilisha kazi yake, ili kwamba muwe watu waliokomaa na wakamilifu msiopungukiwa na kitu cho chote. Hivyo kama mmoja wenu atapungukiwa na hekima, anapaswa kumwomba Mungu anayewapa watu wote kwa ukarimu, naye atampa hekima. Lakini anapaswa kuwa na imani anapoomba pasipo mashaka yo yote, kwani yule aliye na mashaka ni kama wimbi la baharini, linalosukumwa na upepo na kusukwa sukwa. Mtu wa jinsi hiyo asidhani kuwa anaweza kupokea cho chote kutoka kwa Bwana; yeye ni mwenye mashaka na hufikiria mambo mawili tofauti kwa wakati mmoja. Ndugu aliye maskini na awe na furaha sana kwamba Mungu amemchukulia kuwa mtu wa maana sana. Na waaminio walio matajiri wawe na furaha sana tu pale Mungu anapowashusha chini. Kwani utajiri wao hautawazuia kufa kama maua ya porini. Jua linapochomoza na kuwa kali zaidi, joto lake hukausha mimea na maua huanguka chini na kupukutika na kupoteza urembo wake. Kwa jinsi hiyo hiyo, mtu tajiri atafifia katika shughuli zake. Amebarikiwa mtu yule anayestahimili majaribu, maana anapofaulu mitihani atapokea taji yenye uzima ambayo Mungu amewaahidi wale wanaompenda. Yeyote anayejaribiwa hapaswi kusema, “Jaribu hili linatoka kwa Mungu,” kwa sababu maovu hayamjaribu Mungu na hamjaribu mtu yeyote. Bali kila mmoja anajaribiwa na tamaa zake mwenyewe, anapovutwa na kunaswa. Kisha tamaa inapotunga mimba inazaa dhambi, na dhambi ikikomaa kabisa inazaa kifo. Kaka zangu na dada zangu wapendwa msikubali kudanganywa, Kila karama njema na kila tuzo kamilifu hutoka juu; hushuka chini kutoka kwa Baba aliyeumba nuru zote zilizoko mawinguni ambamo kwake yeye hakuna mabadiliko kama vile vivuli vinavyosababishwa na mzunguko wa sayari. Kwa uamuzi wake mwenyewe Mungu alituzaa sisi na kuwa watoto wake kwa njia ya ujumbe wa kweli ili tuwe mazao ya kwanza yenye heshima ya pekee miongoni mwa vyote alivyoviumba. Kumbukeni hili ndugu zangu wapendwa: Kila mtu awe mwepesi wa kusikia lakini awe mzito wa kusema, na mzito kukasirika, kwa sababu hasira ya mwanadamu haitoi haki inayohitajiwa na Mungu toka kwetu. Hivyo acheni matendo yote machafu na kila uovu uliokaa karibu yenu, na mpokee kwa unyenyekevu mafundisho yaliyopandwa ndani ya mioyo yenu. Neno hilo, lina uwezo wa kuleta wokovu wa roho zenu. Usisikilize tu kile ambacho mafundisho ya Mungu yanakisema; bali fanya yale inayosema! Ikiwa utasikiliza tu, utajidanganya mwenyewe. Kwani kama mtu atasikiliza mafundisho ya Mungu, lakini asitende yanayosemwa, yuko kama mtu anayeutazama uso wake kwenye kioo. Anajiangalia mwenyewe kwa haraka na anapoondoka tu husahau anavyoonekana. Lakini anayetazama kwa makini katika sheria kamilifu ya Mungu, inayowaletea watu uhuru, na akaendelea kufanya hivyo asiwe msikilizaji anayesahau, bali huyatunza mafundisho katika matendo, mtu huyo atakuwa na baraka katika kila analofanya. Kama kuna anayedhani kuwa ni mshika dini, lakini bado hauzuii ulimi wake anajidanganya mwenyewe. Dini yake mtu huyu haina manufaa. Dini safi na isiyo na lawama mbele za Mungu Baba, inahusisha haya: kuwatunza yatima na wajane katika mazingira mgumu na kujilinda asichafuliwe na ulimwengu. Kaka zangu na dada zangu, ninyi ni wenye imani katika Bwana wetu mtukufu Yesu Kristo. Kwa hiyo msiwachukulie baadhi ya watu kuwa wa maana zaidi kuliko wengine. Tuchukulie mtu mmoja anakuja katika mkutano wenu akiwa amevaa pete ya dhahabu ama akiwa amevaa mavazi ya thamani, na mtu maskini aliyevaa mavazi yaliyochakaa na machafu naye akaja ndani. Na tuchukulie kuwa mnaonyesha kumjali zaidi yule mtu aliyevaa mavazi mazuri na kusema, “Wewe keti hapa katika kiti hiki kizuri.” Lakini unamwambia yule mtu maskini, “Wewe simama pale,” au, “Keti chini karibu na miguu yetu.” Je, hiyo haioneshi kwamba mnafikiri miongoni mwenu kuwa baadhi ya watu ni bora kuliko wengine? Mmesimama kama mahakimu wenye maamuzi mabaya? Sikilizeni kaka na dada zangu wapendwa! Mungu aliwachagua wale walio maskini machoni pa watu kuwa matajiri katika imani. Aliwachagua kuwa warithi wa Ufalme, ambao Mungu aliwaahidi wale wanaompenda? Lakini ninyi mmewadhalilisha walio maskini! Na kwa nini mnawapa heshima kubwa watu walio matajiri? Hawa ndiyo wale ambao daima wanajaribu kuyadhibiti maisha yenu. Si ndiyo hao wanaowapeleka ninyi mahakamani? Je, si ndiyo hao hao wanaolitukana Jina zuri la Bwana wenu? Kama kweli mnaitunza sheria ya ufalme inayopatikana katika Maandiko, “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe,” mtakuwa mnafanya vizuri. Lakini kama mtakuwa mnaonyesha upendeleo, mtakuwa mnafanya dhambi na mtahukumiwa kuwa na hatia kama wavunja sheria. Ninasema hivi kwa sababu yeyote anayeitunza Sheria yote, lakini akaikosea hata mmoja tu atakuwa na hatia ya kuihalifu Sheria yote. Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,” pia ndiye aliyesema, “Usiue.” Hivyo, kama hutazini lakini ukaua utakuwa umevunja Sheria yote ya Mungu. Mseme na kutenda kama watu watakaokuja kuhukumiwa kwa sheria inayoleta uhuru. Kwa kuwa hukumu ya Mungu haitakuwa na huruma kwake yeye ambaye hakuwa na rehema. Lakini rehema huishinda hukumu! Ndugu zangu, ikiwa mtu atasema kuwa anayo imani lakini hafanyi kitu, imani hiyo haina manufaa yoyote. Imani ya jinsi hiyo haiwezi kumwokoa mtu yeyote. Kama ndugu au dada anahitaji mavazi na anapungukiwa chakula cha kila siku, na ukawaambia, “Mungu awe nanyi! Mkahifadhiwe mahala pa joto na mle vizuri!” Hiyo ina manufaa gani kwao? Usipowapa vitu wanavyovihitaji, maneno yako yanakosa maana! Kwa jinsi hiyo hiyo, imani isipokuwa na matendo itakuwa imekufa. Lakini mtu anaweza kuleta hoja kusema, “Watu wengine wanayo imani, na wengine wanayo matendo mema.” Jibu langu litakuwa, huwezi kunionyesha imani yako pasipo kufanya tendo lolote. Lakini mimi nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Je, mnaamini kwamba kuna Mungu mmoja tu? Vema! Hata mapepo yanaamini na kutetemeka kwa hofu. Wewe mjinga! Je, unahitaji uthibitisho kwamba imani bila matendo haina manufaa? Je, si baba yetu Ibrahimu alihesabiwa haki na Mungu kwa matendo yake alipomtoa sadaka mwanae Isaka juu ya madhabahu? Kwa hakika unaweza kuiona imani hiyo ilifanya kazi pamoja na matendo yake. Kwa hiyo imani yake ilikamilishwa na matendo yake. Ndipo yakatimizwa yale yaliyo kwenye Maandiko kuwa, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na kwa imani hiyo akafanywa kuwa mwenye haki kwa Mungu,” na kwa sababu hiyo akaitwa “Rafiki wa Mungu”. Mnamwona mtu huyo amefanywa kuwa mwenye haki kwa Mungu kwa matendo yake wala siyo kwa imani peke yake. Je, Rahabu yule kahaba si alifanywa kuwa mwenye haki na Mungu kwa matendo aliyofanya, alipowasaidia wale waliokuwa wakipeleleza nchi kwa niaba ya watu wa Mungu. Aliwakaribisha nyumbani mwake na kuwawezesha kutoroka kwa njia nyingine. Hivyo, kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo, imani imekufa ikiwa haina matendo. Kaka na dada zangu, msiwe walimu wengi miongoni mwenu. Mnajua kuwa sisi tulio walimu tutahukumiwa zaidi tena kwa umakini kweli. Ninawatahadharisha kwa sababu sote tunakosa mara kwa mara. Na kama kuna mtu asiyekosa kwa maneno yake, huyo ni mkamilifu, huyo anaweza kuumudu mwili wake wote. Tunawaweka lijamu katika midomo ya farasi, ili waweze kututii sisi. Kwa lijamu hizo tunaweza kuidhibiti miili yao. Au tuchukue meli kama mfano: Hata kama ni kubwa mno na husukumwa na upepo mkali, zinaongozwa kwa usukani mdogo sana na kwenda po pote alikokusudia nahodha kuipeleka. Kwa jinsi hiyo hiyo, ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini unaweza kujivuna kuwa umetenda mambo makubwa sana. Fikiri jinsi ambavyo msitu mkubwa unaweza kuwashwa moto kwa mwali mdogo tu! Ndiyo, ulimi ni mwali wa moto. Ulimi unawakilisha ulimwengu wa uovu miongoni mwa viungo vya mwili wetu. Ulimi huo huo huuchafua mwili wote, na unaweza kuwasha moto maisha yote ya mtu. Nao unapata moto wake kutoka Jehanamu. Aina zote za wanyama na ndege, mijusi na viumbe vya baharini wanaweza kufugwa na wanadamu wamekuwa wanawafuga. Lakini hakuna mtu aliyefaulu kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia na umejaa sumu ya kuua. Kwa ulimi huo tunambariki Bwana na Baba, na kwa huo huo tunawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu! Kutoka katika kinywa hicho hicho hutoka baraka na laana. Kaka na dada zangu, haipaswi kuwa hivyo. Chemichemi ya maji haiwezi kutoa maji matamu na maji machungu kutoka katika tundu moja, je inawezekana? Ndugu zangu, je mtini unaweza kuzaa zeituni? Au mzabibu waweza kuzaa tini? Kwa hakika haiwezekani! Wala chemichemi ya maji chumvi haiwezi kutoa maji matamu. Nani miongoni mwenu aliye na hekima na ufahamu? Na aoneshe hekima yake kwa mwenendo mzuri, kwa matendo yake yanayofanywa kwa unyenyekevu unaoletwa na hekima. Lakini kama mtakuwa na wivu wenye uchungu na ubinafsi ndani ya mioyo yenu, hamwezi kujivunia hekima yenu; kwamba kujivuna kwenu kungekuwa ni uongo unaoficha ukweli. Hii sio aina ya hekima inayotoka juu mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyotoka kwa Roho wa Mungu bali ni ya kishetani. Kwa sababu pale penye wivu na ubinafsi, basi panakuwepo vurugu na kila aina ya matendo maovu. Lakini hekima inayotoka mbinguni juu kwanza juu ya yote ni safi, kisha ni ya amani ina upole na ina busara. Imejaa rehema na huzaa mavuno ya matendo mema. Haina upendeleo wala unafiki. Wale wenye bidii ya kuleta amani na wanaopanda mbegu zao kwa matendo ya amani, watavuna haki kama mavuno yao. Mapigano na magombano yanatokea wapi miongoni mwenu? Je, hayatoki kutoka ndani yenu wenyewe, kutoka katika tamaa zenu za starehe ambazo zinafanya vita siku zote ndani ya miili yenu? Mnataka mambo lakini hamyapati, hivyo mnaua na mnakuwa na wivu juu ya watu wengine. Lakini bado hamwezi kuyafikia mnayoyataka, hivyo mnagombana na kupigana. Nanyi ndugu zangu hampokei mambo mnayoyataka kwa sababu hamumwombi Mungu. Na mnapoomba, lakini hampokei cho chote kwa sababu mnaomba kwa dhamiri mbaya, ili muweze kuvitumia mlivyopatiwa kwa anasa zenu. Watu msio waaminifu, hamjui kwamba kuupenda ulimwengu ni sawa na kumchukia Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hujifanya mwenyewe kuwa adui wa Mungu. Je, kile Maandiko yanachokisema hakina maana yoyote kwenu? Ile roho ambayo Mungu aliifanya ikae ndani yetu wanadamu imejaa tamaa yenye wivu? Lakini Mungu ametuonesha sisi, rehema kuu zaidi. Ndiyo maana Maandiko yanasema: Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa neema wale walio wanyenyekevu. Kwa hiyo jiwekeni chini ya Mungu. Mpingeni Shetani naye atawakimbia ninyi. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Iosheni mikono yenu ninyi wenye dhambi na kuitakasa mioyo yenu enyi wanafiki! Ombolezeni na kulia! Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa maombolezo, na furaha yenu igeuzwe kuwa huzuni kubwa. Jinyenyekezeni chini ya Bwana, naye atawainua juu. Ndugu, msiendelee kukosoana ninyi kwa ninyi. Yeye anayemnenea mabaya ndugu yake au anayemhukumu ndugu yake atakuwa anailaumu Sheria na atakuwa anaihukumu Sheria. Na kama utaihukumu Sheria, hautakuwa unafanya yale yanayosemwa na Sheria, bali utakuwa ni hakimu. Kuna Mtoa Sheria mmoja tu na hakimu, ndiye Mungu aliye na uwezo wa kuokoa na kuangamiza. Hivyo wewe unafikiri ni nani, wewe unayemhukumu jirani yako? Sikilizeni mnaosema, “Leo au kesho tutasafiri kwenda kwenye mji huu au ule, na tutakaa mwaka mzima pale, tutafanya biashara hapo na kujipatia fedha nyingi.” Hamjui hata yatakayotokea katika maisha yenu kesho yake tu. Kwani ninyi ni mvuke tu ambao huonekana kwa kipindi kifupi tu kisha hutoweka. Badala yake, nyakati zote mngesema, “Kama Bwana anapenda, tutaishi na tutafanya hivi au vile.” Kama ilivyo, ninyi mna kiburi na kujivuna. Majivuno yote ya jinsi hiyo ni uovu! Hivyo sasa, mnaposhindwa kufanya mliyoyajua ni haki, mtakuwa na hatia ya dhambi. Sikilizeni, ninyi matajiri! Ombolezeni na kulia kwa sauti kwa ajili ya dhiki inayowajia. Utajiri wenu umeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu zenu na fedha vimeliwa na kutu! Hiyo kutu itakuwa ni ushuhuda dhidi yenu, na itaila miili yenu kama kwa moto. Mmejilimbikizia mali kwa ajili yenu katika kizazi hiki cha siku za mwisho! Angalieni! Mmeyazuia malipo ya wafanyakazi waliopalilia mashamba yenu. Sasa wananililia! Na kilio cha hao wanaovuna pia kimeyafikia masikio ya Bwana Aliye na Nguvu. Mmeishi maisha ya anasa duniani na kujifurahisha na kila kitu mlichotaka. Mmeinenepesha miili yenu, kama wanyama walio tayari kwa siku ya kuchinjwa. Mmehukumu na kuua wale watu wasio na hatia, na ambao hawakupingana nanyi. Hivyo kina kaka na kina dada, muwe na subira; hadi kuja kwa mara ya pili kwa Bwana. Kumbukeni kuwa mkulima huyasubiria mazao yake yenye thamani yakue ardhini. Huyangoja kwa subira mpaka yapate mvua za masika na za vuli. Hata ninyi pia mnapaswa kungoja kwa subira. Muwe imara mioyoni mwenu, kwa sababu kuja kwa Bwana mara ya pili kumekaribia. Kaka na dada zangu, msiendelee kunung'unikiana ninyi kwa ninyi, ili msije kuhukumiwa kuwa na hatia. Tazameni! Hakimu anasimama mlangoni akiwa tayari kuingia ndani. Kina kaka na kina dada, fuateni mfano wa manabii waliosema kwa jina la Bwana. Wao walipata mateso mengi mabaya lakini walivumilia. Na tunatoa heshima kubwa sana kwa wale wote waliostahimili mateso. Mmesikia juu ya uvumilivu wa Ayubu, na mnayajua ya kuwa baada ya yote hayo Bwana alimsaidia. Hii basi inaonesha ya kuwa Bwana ni mwenye wingi wa rehema na huruma. Juu ya mambo yote kaka zangu na dada zangu, usitumie kiapo unapotoa ahadi, Usiape kwa mbingu wala kwa dunia, ama kwa kitu kingine chochote. “Ndiyo” yenu na iwe “Ndiyo halisi”, na “Hapana” yenu na iwe “Hapana halisi”, ili msije mkaingia katika hukumu ya Mungu. Je, miongoni mwenu kuna aliye na shida? Anapaswa kuomba. Je, yupo yeyote mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. Je, kuna yeyote kwenu aliye mgonjwa? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa kumwombea na kumpaka mafuta katika jina la Bwana. Maombi yanayofanywa kwa imani yatamfanya mgonjwa apone, na Bwana atampa uzima. Kama atakuwa ametenda dhambi, Bwana atamsamehe. Hivyo muungame dhambi ninyi kwa ninyi, na kuombeana ninyi kwa ninyi ili muweze kuponywa. Maombi yanayofanywa na mtu mwenye haki yana nguvu sana na yana matokeo makubwa sana. Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi tulivyo. Aliomba kwamba mvua isinyeshe, na haikunyesha katika ardhi kwa miaka mitatu na nusu. Kisha akaomba tena inyeshe, na anga ikatoa mvua, na ardhi ikatoa mazao. Kaka na dada zangu Ndugu zangu, kama mmoja wenu atapotoka katika kweli, na mwingine akamrejeza, yule aliyemrejeza atambue kuwa yule anayemrejeza mtenda dhambi kutoka katika njia yake mbaya ataiokoa roho ya huyo mtu kutoka katika kifo cha milele na atasababisha dhambi nyingi zisamehewe. Kutoka kwa Petro, mtume wa Yesu Kristo. Kwa wateule wa Mungu, ambao huonekana kama ni wageni kutoka nchi nyingine, waliotawanyika katika majimbo yote ya Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia, na Bithinia. Kwa kadri ya mpango wa Mungu Baba alioufanya muda mrefu uliopita, mliteuliwa muwe wake kwa kufanywa watakatifu na Roho Mtakatifu. Mliteuliwa kuwa waatiifu kwa Mungu na kutakaswa na kujumuishwa miongoni mwa watu wa Agano Jipya kwa kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani ya Mungu viwe pamoja nanyi kwa wingi. Atukuzwe Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Katika rehema zake kuu, Mungu alitufanya sisi tuzaliwe upya ili tuwe na tumaini lililo hai, kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo kutoka kwa waliokufa, na ili kuwa na urithi usioharibika, ulio safi na usiofifia, uliotunzwa kwa ajili yenu kule mbinguni. Ni kwa ajili yenu ninyi ambao kwa njia ya imani, mnalindwa na nguvu za Mungu ili mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho. Hili linawafanya mfurahi sana, hata kama kwa sasa imewalazimu mhuzunishwe kwa kipindi kifupi kwa masumbufu na mateso ya aina mbali mbali. Kwa masumbufu haya imani yenu inajaribiwa na kuithibitishwa kuwa ni ya kweli. Hii inafananishwa na dhahabu pale inapopitishwa kwenye moto kuthibitisha uhalisi wake. Lakini hata dhahabu ya kweli inaweza kuharibiwa. Hivyo imani ina thamani zaidi kuliko dhahabu. Pale imani yenu inapothibitika kuwa ni ya kweli, matokeo yake ni sifa, utukufu na heshima kwa Mungu wakati wa kurudi kwake Yesu Kristo. Hata kama hamjamwona Yesu, lakini mnampenda. Hata kama hamuwezi kumuona kwa sasa, lakini mnamwamini yeye na mmejazwa na furaha ya ajabu isiyoweza kuelezwa kwa maneno. Mnaupokea wokovu wenu ambao ni lengo la imani yenu. Manabii waliotabiri juu ya neema ambayo ingeoneshwa kwenu, walipeleleza kwa makini na kwa uangalifu wakaulizia habari za wokovu huu. Roho wa Kristo alikuwa ndani yao, naye aliwapa ushuhuda mapema kuhusu Kristo kwamba itamlazimu kuteswa na baada ya hapo atapokea utukufu. Manabii waliuliza kutaka kujua wakati gani na katika mazingira gani mambo haya yangetokea. Ilifunuliwa kwao kwamba walikuwa hawajitumikii wenyewe. Badala yake, waliwatumikia ninyi walipotabiri juu ya mambo haya. Na sasa mmesikia juu ya mambo haya kutoka kwa wale waliyowaambia habari Njema kwa msaada wa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wangetamani sana kufahamu zaidi juu ya mambo haya mliyoambiwa. Hivyo mkeshe katika fahamu zenu na kuwa na kiasi. Yawekeni kikamilifu matumaini yenu katika baraka mtakazopewa wakati Yesu Kristo atakapofunuliwa. Kama watoto watiifu, msiyaache maisha yenu yandelee kutawaliwa na tamaa mbaya mlizokuwa nazo awali mlipokuwa wajinga. Badala yake, kama ambavyo yeye Mungu aliyewaita alivyo mtakatifu, hata ninyi muwe watakatifu katika kila mnalotenda. Hivyo Maandiko yanasema: “Iweni watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu.” Na kama Baba mnayemwita Mungu anayewahukumu watu bila upendeleo kwa kadri ya matendo ya kila mtu, muishi maisha ya utauwa na hofu kwa Mungu katika miaka yenu ya kukaa humu duniani kama wageni. Mnajua kwamba siyo kwa mambo yaharibikayo kama fedha au dhahabu, kwamba mliokolewa kutoka katika maisha yasiyofaa mliyoyapokea kutoka kwa babu zenu, bali kwa damu ya thamani ya Kristo, kama ile ya mwanakondoo asiye na dosari wala ila. Kristo alichaguliwa kabla ya uumbaji wa ulimwengu, lakini alidhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. Kupitia Kristo mmekuwa waamini katika Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na kumpatia utukufu. Ili imani yenu na matumaini yawekwe katika Mungu. Sasa kwa vile mmejitakasa wenyewe kwa kuitii kweli hadi mwisho kwamba mtaonesha upendo wa kweli wa kindugu, jitahidini kupendana ninyi kwa ninyi kwa mioyo iliyo safi. Mmezaliwa upya sio kama matokeo ya mbegu inayoharibika, lakini kama matokeo ya mbegu isiyoharibika. Mmezaliwa upya kwa njia ya ujumbe wa Mungu, ambao unaleta uzima ndani yenu. Hivyo, kama Maandiko yanavyosema: “Watu wote ni kama manyasi, na utukufu wao wote ni kama maua pori katika manyasi. Manyasi yananyauka na kukauka, na maua yanapukutika, bali ujumbe wa Bwana unadumu milele.” Na ujumbe huo ni habari njema iliyohubiriwa kwenu. Hivyo acheni uovu wote, pamoja na uongo, hali za unafiki na wivu na aina zote za kashfa. Kama watoto wachanga, mnapaswa kuyatamani maziwa ya kiroho yaliyo safi, ili kwa ajili ya hayo muweze kukua na kuokolewa, kwa vile mmekwisha kuujaribu wema wa Bwana. Mkaribieni Bwana Yesu, aliye Jiwe lililo Hai, lililokataliwa na watu, bali kwa Mungu ni jiwe lililoteuliwa na kuheshimika. Ninyi pia, kama mawe yaliyo hai mnajengwa ili kuwa hekalu la kiroho. Mmekuwa makuhani watakatifu mkimtumikia Mungu kwa kutoa sadaka za kiroho zinazokubalika kwake kwa njia ya Yesu Kristo. Hivyo, Maandiko yanasema, “Tazameni, naweka katika Sayuni Jiwe la msingi katika jengo, lililoteuliwa na kuheshimika, na yeyote anayeamini hataaibishwa.” Inamaanisha heshima kwenu mnaoamini, bali kwa wasioamini, “jiwe walilolikataa wajenzi limekuwa jiwe la muhimu kuliko yote.” Na, “jiwe linalowafanya watu wajikwae na mwamba unaowafanya watu waanguke.” Walijikwaa kwa sababu hawakuutii ujumbe wa Mungu, na Mungu alisema hilo litatokea wasipotii. Lakini ninyi ni watu mlioteuliwa, ni Ukuhani unaomtumikia Mfalme. Ninyi ni taifa takatifu nanyi ni watu wa Mungu. Yeye aliwaita Ili muweze kutangaza matendo yake yenye nguvu. Naye aliwaita mtoke gizani na mwingie katika nuru yake ya ajabu. Kuna wakati hamkuwa watu, lakini sasa mmekuwa watu wa Mungu. Kuna wakati hamkuoneshwa rehema, lakini sasa mmeoneshwa rehema za Mungu. Rafiki zangu, ninawasihi kama wapitaji na wageni katika ulimwengu huu kuwa mbali na tamaa za kimwili, ambazo hupingana na roho zenu. Muwe na uhakika wa kuwa na mwenendo mzuri mbele ya wapagani, ili hata kama wakiwalaumu kama wakosaji, watayaona matendo yenu mazuri nao wanaweza kumpa Mungu utukufu katika Siku ya kuja kwake. Nyenyekeeni kwa mamlaka yo yote ya kibinadamu kwa ajili ya Bwana. Mnyenyekeeni mfalme, aliye mamlaka ya juu kabisa. Na muwatii viongozi waliotumwa na mfalme. Wametumwa ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale wanaofanya mazuri. Kwa kuwa mapenzi ya Mungu ni kwamba, kwa kutenda mema mtayanyamazisha mazungumzo ya kijinga ya watu wasio na akili. Muishi kama watu walio huru, lakini msiutumie uhuru huo kama udhuru wa kufanya maovu. Bali muishi kama watumishi wa Mungu. Onesheni heshima kwa watu wote: Wapendeni ndugu zenu na dada zenu waliomo nyumbani mwake Mungu. Mcheni Mungu na mumheshimu mfalme. Watumwa mlio nyumbani, watumikieni mabwana wenu kwa heshima yote, siyo tu wale walio wapole na wenye busara, bali hata wale walio wakali. Baadhi yenu mtapata mateso wakati ambapo hamjafanya kosa lolote. Ikiwa utaweza kuvumilia maumivu na kuweka fikra zako kwa Mungu, hilo linampendeza sana Mungu. Kwani kuna sifa gani iliyopo kwako kama utapigwa kwa kutenda mabaya na kuvumilia? Lakini kama utateseka kwa kutenda mema na kustahimili, hili lampendeza Mungu. Ni kwa kusudi hili mliitwa na Mungu, kwa sababu Kristo pia aliteseka kwa ajili yenu na kwa kufanya hivyo aliacha kielelezo kwenu, ili tuweze kuzifuata nyayo zake. “Hakutenda dhambi yo yote, wala hakukuwa na udanganyifu uliopatikana kinywani mwake.” Alipotukanwa hakurudishia matusi. Alipoteseka, hakuwatishia, bali wakati wote alijitoa mwenyewe kwa Mungu ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu kwenye mwili wake hadi pale msalabani, ili tuweze kuacha kuishi kwa ajili ya dhambi na kuishi kwa ajili ya haki. Ilikuwa ni kwa njia ya majeraha yake kwamba mliponywa. Kwani mlikuwa kama kondoo wanaotangatanga huko na huko, lakini sasa mmerudi kwa Mchungaji na Mwangalizi wa maisha yenu. Vivyo hivyo, enyi wake mnapaswa kuwa radhi kuwahudumia waume zenu. Ili hata wale waliokataa kuyapokea mafundisho ya Mungu washawishike na kuamini kutokana na jinsi mnavyoishi. Hivyo hamtahitaji kusema chochote. Waume zenu watayaona maisha safi mnayoishi yanayomheshimu Mungu. Si nywele za gharama, vito vya dhahabu, au nguo nzuri zitakazowafanya mpendeze. Bali, uzuri wenu utoke ndani yenu, uzuri wa roho yenye upole na utulivu. Uzuri huo hautatoweka kamwe. Ni wa thamani sana kwa Mungu. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa wanawake watakatifu walioishi hapo zamani na kumfuata Mungu. Walijipamba kwa jinsi hiyo hiyo kwa kuwahudumia waume zao. Ninazungumza juu ya wanawake kama Sara aliyemtii Ibrahimu, mume wake na kumwita bwana wake. Na ninyi wanawake ni watoto wa kweli wa Sara ikiwa daima mnafanya yale yaliyo sahihi pasipokuwa na hofu. Vivyo hivyo, enyi waume inawapasa kuishi na wake zenu kwa kuelewa udhaifu alionao mwanamke na matumaini ya Mkristo. Hamna budi kuwapa heshima kwa sababu Mungu kwa sababu Mungu anawapa baraka zile zile anazowapa ninyi, yaani neema ya maisha ya kweli. Fanyeni hivi ili maombi yenu yasizuiliwe. Hivyo ninyi nyote mnapaswa kuishi pamoja kwa amani. Mjitahidi kuelewana ninyi wenyewe. Mpendane kama kaka na dada na muwe wanyenyekevu na wema. Msimfanyie uovu mtu yeyote ili kulipa kisasi kwa uovu aliowatendea. Msimtukane mtu yeyote ili kulipiza matusi aliyowatukana. Lakini mwombeni Mungu awabariki watu hao. Fanyeni hivyo kwa sababu ninyi wenyewe mliteuliwa kupokea baraka, Maandiko yanasema: “Anayetaka kufurahia maisha ya kweli na kuwa na siku nyingi njema tu, aepuke kusema chochote kinachoumiza, na asiruhusu uongo utoke kwenye kinywa yake. Aache kutenda uovu, na atende mema. Atafute amani, na fanya kila analoweza ili kuwasaidia watu kuishi kwa amani. Bwana huwaangalia wale watendao haki, na husikia maombi yao. Lakini yu kinyume cha wale watendao uovu.” Ikiwa unajaribu kwa bidii kutenda mema, ni nani atakayetaka kukudhuru? Lakini hata ukiteseka kwa sababu kutenda yaliyo haki, unazo Baraka za Mungu. “Msimwogope mtu yeyote, wala msiruhusu watu wawasumbue.” Lakini mjitoe kikamilifu kwa Kristo ambaye ni Bwana wenu pekee. Na daima iweni tayari kumjibu mtu yeyote anayetaka ufafanuzi kuhusu tumaini linaloyaongoza maisha yenu. Lakini wajibuni kwa upole na heshima kwa ajili ya Mungu, mkizitunza dhamiri zenu mbele zake. Ndipo watu watakapoona namna njema mnayoishi kama wafuasi wa Kristo. Na wataaibika kwa kuwanenea mabaya. Ni afadhali kuteseka kwa kutenda mema kuliko kutenda mabaya. Ndiyo, ni bora ikiwa hivyo ndivyo Mungu anavyotaka. Kristo mwenyewe aliteseka alipokufa kwa ajili yenu, na kwa kifo hicho kimoja alilipa fidia kwa ajili ya dhambi. Hakuwa na hatia, lakini alikufa kwa ajili ya watu waliokuwa na hatia. Alifanya hivyo ili awalete ninyi nyote kwa Mungu. Kama mwanadamu, aliuawa, lakini uhai wake ulifanywa hai na Roho. Na kwa Roho alikwenda akazihubiri roho zilizo kifungoni. Hizo ndizo roho zilizokataa kumtii Mungu hapo zamani wakati wa Nuhu. Mungu alisubiri kwa uvumilivu Nuhu alipokuwa anaunda safina. Na watu wachache tu, yaani wanane kwa jumla ndiyo walioingia katika safina na kuokolewa kwa kuvushwa salama katika gharika hiyo. Na maji yale ni kama ubatizo, unaowaokoa ninyi sasa kupitia ufufuo wa Yesu Kristo kutoka katika wafu na siyo kuondoa uchafu mwilini kwa kuoga. Ni ahadi ya dhati ya kuishi kwa kumcha Mungu. Sasa yupo mbinguni upande wa kuume wa Mungu, na anatawala juu ya malaika, mamlaka na nguvu. Kristo aliteseka alipokuwa katika mwili wake. Hivyo mjitayarishe kwa fikra ile ile aliyokuwa nayo Kristo. Yeyote anayekubali kuteseka katika maisha haya hakika ameamua kuacha kutenda dhambi. Jiimarishe wenyewe ili mweze kuishi maisha yenu yaliyosalia hapa duniani kwa kutenda yale anayotaka Mungu, siyo maovu ambayo watu wanataka kufanya. Huko nyuma mmepoteza muda mwingi mkitenda yale ambayo wasiyomjua Mungu wanapenda kutenda. Mliishi kwa kutojali maadili, mkitenda maovu mliyotaka kutenda. Daima mlikuwa mnalewa, mlifanya sherehe mbaya za ulevi, na mlitenda mambo ya aibu katika ibada zenu za sanamu. Na sasa “marafiki” zenu wa zamani wanaona ni ajabu kwamba ninyi hamshirikiani nao katika njia za maisha zilizo mbaya na zisizofaa wanazozifuata. Na hivyo wanasema mabaya juu yenu. Lakini itawalazimu kukutana na Mungu na kutoa maelezo juu ya yale waliyoyatenda. Yeye ndiye atakaye hukumu watu wote muda si mrefu, walio hai sasa na wale waliokwisha kufa. Walikosolewa na wengine katika maisha yao hapa duniani. Lakini ulikuwa mpango wa Mungu kwamba wasikie Habari Njema kabla hawajafa ili wawe na maisha mapya katika Roho. Wakati wa kila kitu kufikia mwisho wake umekaribia. Hivyo iweni waangalifu katika akili zenu na mjizuie kwa kila jambo. Hii itawasaidia katika maombi yenu. Jambo lililo muhimu kuliko yote, daima mpendane ninyi kwa ninyi kikamilifu, kwa sababu upendo huwawezesha kusamehe dhambi. Mkaribishane ninyi kwa ninyi katika nyumba zenu na kushiriki chakula kwa pamoja pasipo manunguniko. Mungu amewapa neema yake kwa namna nyingi mbalimbali. Hivyo muwe watumishi wema na kila mmoja wenu atumie kipawa chochote alichopewa kwa njia iliyo bora katika kuhudumiana ninyi kwa ninyi. Ikiwa kipawa chako ni kuhubiri, maneno yako yawe kama yanayotoka kwa Mungu. Ikiwa kipawa chako ni kuhudumu, unatakiwa kuhudumu kwa nguvu anazokupa Mungu. Ndipo Mungu atakaposifiwa kwa kila jambo katika Yesu Kristo. Uwezo na utukufu ni wake milele na milele. Amina. Rafiki zangu, msishangae kwa sababu ya mateso mnayoyapata sasa, mateso hayo yanaijaribu imani yenu. Msidhani kuwa linalotokea kwenu ni jambo la ajabu. Lakini mnapaswa kufurahi kwa kuwa mnayashiriki mateso ya Kristo. Mtafurahi na kujawa na raha wakati uweza wake mkuu utapodhihirishwa kwa ulimwengu. Mhesabu kuwa ni heshima watu wanapowanenea mabaya kwa sababu mnamwakilisha Kristo. Linapotokea hilo inaonesha kuwa Roho wa Mungu, aliye Roho wa utukufu, yupo pamoja nanyi. Mnaweza kupata mateso; lakini msiteseke kwa sababu mmeua, mmeiba, mmesababisha ghasia, au mmejaribu kutawala maisha ya watu wengine. Lakini endapo utateswa kwa kuwa ni “Mkristo” basi usione haya. Bali umshukuru Mungu kwa kuwa unalibeba jina hilo. Wakati wa kuanza hukumu umewadia. Hukumu hiyo itaanza na familia ya Mungu. Ikiwa itaanzia kwetu, nini kitawatokea wale wasioikubali Habari Njema ya Mungu? “Iwapo ni vigumu hata kwa mtu mwema kuokolewa, nini kitatokea kwa yule aliye kinyume na Mungu na amejaa dhambi?” Hivyo kama mnateseka kwa sababu ya kutii mapenzi ya Mungu, yakabidhini maisha yenu kwake maana Yeye ndiye aliyewaumba, na hivyo mnapaswa kumwamini. Na anastahili kuthaminiwa na kuaminiwa. Sasa nina jambo la kuwaambia wazee walio katika kundi lenu. Mimi pia ni mzee nami mwenyewe nimeyaona mateso ya Kristo. Na nitashiriki katika utukufu utakaodhihirishwa kwetu. Hivyo ninawasihi, mlitunze kundi la watu mnalowajibika kwalo. Ni kundi lake Mungu. Basi lichungeni kwa moyo wa kupenda na si kwa kulazimishwa. Hivi ndivyo Mungu anavyotaka. Fanyeni hivyo kwa sababu mnafurahi kutumika, na si kwa sababu mnataka pesa. Msiwaongoze wale mnaowasimamia kwa kuwaamrisha. Lakini muwe mfano mzuri wa kuiga kwao. Ili Kristo aliye Mchungaji Mkuu atakapokuja, mpate taji yenye utukufu na isiyopoteza uzuri wake. Vijana, nina jambo la kuwaambia ninyi pia. Mnapaswa kutii mamlaka ya wazee. Na ninyi nyote mnapaswa kuwa wanyenyekevu ninyi kwa ninyi. “Mungu yu kinyume na wanaojivuna, lakini ni mwema kwa wanyenyekevu.” Hivyo mjinyenyekeze chini ya mkono wa Mungu wenye nguvu. Kisha, wakati sahihi utakapofika, atawalipa kwa kuwainua. Mpeni Mungu masumbufu yenu yote, kwa sababu Yeye anawajali. Iweni na kiasi na muwe waangalifu! Shetani ni adui yenu naye huzunguka zunguka kama simba anayeunguruma akimtafuta yeyote wa kumshambulia na kumla. Mpingeni ibilisi. Kisha msimame imara katika imani yenu. Mnafahamu kwamba ndugu zenu ulimwenguni kote wanapitia mateso sawa na hayo mliyonayo. Ndiyo, mtateseka kwa muda mfupi. Lakini baada ya hapo, Mungu ataweka kila kitu sawa. Atawatia nguvu, atawasaidia na kuwashika msianguke. Yeye ni Mungu ndiye chanzo cha neema yote. Aliwachagua mshiriki katika utukufu wake ndani ya Kristo. Utukufu huo utadumu milele. Uwezo wote ni wake milele. Amina. Sila ataileta barua hii kwenu. Nafahamu kwamba ni ndugu mwaminifu katika familia ya Mungu. Niliandika barua hii fupi kuwatia moyo na kuwaambia kuwa hii ni neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo. Kanisa lililoko Babeli linatuma salamu kwenu. Wameteuliwa kama ninyi. Marko, ambaye ni kama mwanangu kwangu katika Kristo, anawasalimu pia. Mpeni kila mmoja wenu salamu maalumu mnapokutana. Amani iwe kwenu ninyi nyote mlio katika Kristo. Salamu kutoka kwa Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo. Kwenu ninyi nyote mliopokea imani inayowapa baraka sawa nasi. Mlipewa imani kwa sababu Mungu wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo hufanya yaliyo mema na haki. Mpewe neema na amani zaidi na zaidi, kwa sababu sasa mnamjua Mungu na Yesu Bwana wetu. Yesu ana nguvu ya Mungu. Na nguvu yake imetupa heshima ili tuishi maisha yanayomtukuza na kumpendeza Mungu. Tuna vitu hivi kwa sababu tunamjua. Yesu alitualika kwa utukufu na nguvu ya uungu wake. Na kupitia haya, alitupa ahadi kuu mno. Ili kwamba kwa hizo mnaweza kushiriki katika kuwa kama Mungu na ukaepuka maangamizo ya kiroho yanayokuja kwa watu ulimwenguni kwa sababu ya mambo maovu wanayotaka. Kwa sababu mna baraka hizi, jitahidini kadri mnavyoweza kuongeza mambo haya: katika imani yenu ongezeni wema, katika wema wenu ongezeni maarifa; katika maarifa yenu ongezeni kiasi; katika kiasi chenu ongezeni uvumilivu; katika uvumilivu wenu ongezeni kumwabudu Mungu; katika kumwabudu Mungu kwenu ongezeni huruma kwa ndugu katika Kristo na kwa wema huu ongezeni upendo. Ikiwa mambo haya yote yatakaa ndani yenu na kukua, mtazaa matunda mazuri yakiwa ni matokeo ya ninyi kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini wale wasiokua na sifa hizi ndani yao ni wasiyeona. Hawataweza kuona kwa uwazi yale waliyonayo. Wamesahau kuwa dhambi zao ziliondolewa kutoka kwao na wakawa safi. Ndugu zangu, Mungu aliwaita na akawachagua ili muwe wake. Jitahidini mhakikishe kuwa mnapata yale aliyonayo Mungu kwa ajili yenu. Mkifanya hivi hamtajikwa na kuanguka. Na mtakaribishwa kwa baraka kuu katika ufalme usio na mwisho, ufalme wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Mnayajua mambo haya tayari. Mko imara katika kweli mliyo nayo. Lakini daima nitajitahidi kuwakumbusha. Nikiwa bado naishi hapa duniani, nadhani ni sahihi kwangu kuwakumbusha. Ninajua kuwa ni lazima nitauacha mwili huu kitambo kijacho kwani Bwana wetu Yesu Kristo amenionyesha. Nitafanya kwa kadri ninavyoweza kuhakikisha kuwa daima mtayakumbuka mambo haya hata baada ya kifo changu. Tuliwaambia kuhusu nguvu ya Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake katika nguvu kuu. Mambo tuliyowaambia hayakuwa simulizi za kuvutia zilizotungwa watu. Hapana, tuliuona ukuu wa Yesu kwa macho yetu wenyewe. Yesu aliisikia sauti ya Mungu Mkuu na Mwenye Mtukufu alipopokea heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba. Sauti ilisema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda. Ninafurahishwa naye.” Nasi tuliisikia sauti hiyo. Sauti hiyo ilitoka mbinguni tulipokuwa na Yesu juu ya mlima mtakatifu. Hili linatufanya tuwe na ujasiri kwa yale waliyosema manabii. Na ni vizuri ninyi mkifuata yale waliyosema, ambayo ni kama mwanga unaoangaza mahali penye giza. Mna mwanga unaoangaza mpaka siku inapoanza na nyota ya asubuhi huleta mwanga mpya katika fahamu zenu. Jambo la muhimu kuliko yote ambalo ni lazima mlielewe ni hili ya kwamba hakuna unabii katika Maandiko unaotokana na mawazo ya nabii. Nabii hakusema kile alichotaka kusema. Lakini wanadamu waliongozwa na Roho Mtakatifu kusema ujumbe uliotoka kwa Mungu. Hapo zamani walikuwepo manabii wa uongo miongoni mwa watu wa Mungu. Ndivyo itakavyokuwa miongoni mwenu hata sasa. Watakuwepo walimu wa uongo katika kundi lenu, watakaoingiza mawazo yao wenyewe yatakayowaangamiza watu. Na watafundisha kwa werevu ambao mtashindwa kujua kuwa ni waongo. Watakataa hata kumtii Bwana aliwanunua. Na hivyo watajiangamiza haraka wao wenyewe. Watu wengi watawafuata katika mambo madaya ya kimaadili wanayotenda. Na kwa sababu yao, wengi wataikashifu njia ya kweli tunayoifuata. Manabii hawa wa uongo wanachotaka ni pesa zenu tu. Hivyo watawatumia ninyi kwa kuwaambia mambo yasiyo ya kweli. Lakini hukumu ya walimu hawa wa uongo imekwisha andaliwa kwa muda mrefu wala hawatakwepa. Mungu atawaangamiza, hajalala usingizi. Malaika walipotenda dhambi, Mungu hakuwaacha bila kuwaadhibu. Aliwatupia kuzimu. Aliwaweka malaika wale katika mapango yenye giza, wanakofungiwa mpaka wakati watakapohukumiwa na Mungu. Na Mungu aliwaadhibu watu waovu walioishi zamani. Alileta gharika katika ulimwengu uliojaa watu waliokuwa kinyume na Mungu. Lakini alimwokoa Nuhu na watu wengine saba waliokuwa pamoja naye. Nuhu ndiye aliyewaambia watu kuhusu kuishi kwa haki. Pia, Mungu aliiadhibu miji miovu ya Sodoma na Gomora. Aliichoma kwa moto mpaka kila kitu kikawa majivu. Alitumia miji hiyo kama mfano wa kile kitakachowapata watu walio kinyume na Mungu. Lakini alimwokoa Lutu, mtu mwema aliyeishi huko. Lutu aliugua sana moyoni kutokana na mwenendo wa kimaisha usiofaa na matendo ya uasi ya wale watu. Kila siku mtu huyu mwema aliishi miongoni mwa watu walioharibika, na moyo wake mwema uliumia kutokana na uhalifu na uvunjaji wa sheria aliyouona na kusikia. Unaona namna ambavyo Mungu anajua kuwaokoa wale wanaomheshimu kutokana na matatizo yao. Na Bwana anajua jinsi ya kuwaweka watu waovu kifungoni hadi atakapowaadhibu siku ya hukumu. Hukumu hiyo ni kwa wale ambao daima wanaofuata tamaa za udhaifu wao wa kibinadamu. Hiyo ni kwa ajili ya wale ambao wanadharau mamlaka ya Bwana. Walimu hawa wa uongo hufanya chochote wanachotaka, na hujivuna sana. Wala hawaogopi kuwanenea mabaya viumbe wenye nguvu walioko angani. Malaika wa Mungu ni hodari zaidi na wana nguvu kuliko viumbe hawa. Lakini hata hivyo malaika hao wa Mungu hawawatukani na kuwanenea mabaya viumbe hawa mbele za Bwana. Lakini walimu hawa wa uongo wanasema uovu dhidi ya mambo wasiyoyaelewa. Wako kama wanyama ambao hufanya mambo bila ya kufikiri, ni kama wanyama wa porini waliozaliwa ili wakamatwe na kuuawa. Nao kama wanyama wataangamizwa. Wamesababisha watu wengi kuteseka. Hivyo hata wao watateseka. Hayo ndiyo malipo yao kwa yale waliyofanya. Wanadhani ni jambo la kufurahisha kutenda dhambi ambapo kila mtu anaweza kuwaona. Wanazifikiria sherehe zenye matendo yasiyofaa hata wakati wa mchana kweupe. Hivyo wao ni kama madoa ya uchafu na ni fedheha mnapokula pamoja nao. Kila wakati wanapomwona mwanamke, wanamtamani na kumtaka. Wanatenda dhambi kwa njia hii daima. Na wanawasababisha wanyonge kutenda dhambi. Wamejifunza vyema wao wenyewe kuwa walafi. Wako chini ya laana. Walimu hawa wa uongo waliiacha njia sahihi na wakaiendea njia mbaya. Waliifuata njia ile ile aliyoifuata Balaamu. Alikuwa mwana wa Beori, aliyependa kulipwa kwa kufanya mabaya. Alikemewa na punda kwa sababu alikuwa anatenda jamba baya. Punda alizungumza kwa sauti ya kibinadamu na akamzuia nabii yule kutenda kwa wazimu. Walimu hawa wa uongo ni kama chemichemi zisizo na maji. Ni kama mawingu yanayosukumwa na dhoruba. Mahali penye giza nene pameandaliwa kwa ajili yao. Wanajisifu kwa maneno yasiyo na maana. Wanawaongoza watu katika mitego ya dhambi. Wanawatafuta watu ambao wamechana na maisha ya kutenda dhambi na wanawarudisha tena katika kutenda dhambi. Wanafanya hivi kwa kutumia mambo ya aibu ambayo watu wanataka kuyatenda katika mapungufu yao ya kibinadamu. Walimu hawa wa uongo wanawaahidi watu hao uhuru, lakini wao wenyewe hawako huru. Ni watumwa wa akili iliyoharibiwa na dhambi. Ndiyo, watu ni watumwa wa kitu chochote kinachowashinda. Watu wanaweza kuwekwa huru ulimwenguni kutoka katika matendo ya aibu. Wanaweza kuyakwenda haya kwa kumwamini Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Lakini wakiyarudia maovu hayo na yakawatawala, hali yao inakuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzoni. Ndiyo, ingekuwa bora kwao kutoijua kamwe njia sahihi. Ingekuwa bora kuliko kuijua njia sahihi kisha kugeuka kutoka katika mafundisho matakatifu waliyopewa. Walichofanya ni kama “Mbwa anayekula matapishi yake.” Na “Kama nguruwe aliyeoshwa, kisha anarudi kugaagaa matopeni.” Rafiki zangu, hii ni barua yangu ya pili kuwaandikia. Barua zote mbili nimewaandikia ili kusaidia fikra zenu njema zikumbuke kitu. Ninataka mkumbuke maneno ambayo manabii watakatifu walisema huko nyuma. Na mkumbuke amri ambayo Bwana na Mwokozi wetu aliwapa. Aliwapa amri hiyo kupitia mitume wake waliowafundisha. Ni muhimu kwenu kuelewa kitakachotokea siku za mwisho. Watu watawacheka kwa yale mliyofundishwa. Wataishi kwa kufuata maovu wanayotaka kufanya. Watasema, “Yesu aliahidi kuwa atarudi. Yuko wapi? Baba zetu wamekufa, lakini ulimwengu unaendelea kama ambavyo umekuwa tangu ulipoumbwa.” Lakini watu hawa hawataki kukumbuka kilichotokea zamani. Anga ilikuwepo, na Mungu aliiumba dunia kwa kutumia maji. Hili lilitokea kwa neno la Mungu. Kisha ulimwengu uliangamizwa kwa maji wakati wa gharika. Na neno hilo hilo la Mungu linaiweka anga na dunia tuliyonayo sasa. Vimewekwa ili vichomwe moto. Vimewekwa kwa ajili ya siku ya hukumu na kuangamia kwa watu wote walio kinyume na Mungu. Lakini rafiki zangu wapendwa msisahau jambo hili moja ya kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu moja, na miaka elfu moja ni kama siku moja. Bwana hakawii kufanya alichoahidi kama ambavyo watu wengine wanaelewa maana ya kukawia. Lakini Bwana amewavumilia. Hataki mtu yeyote aangamie. Anataka kila mtu abadili njia zake na aache kutenda dhambi. Lakini siku atakayorudi Bwana itakuwa siku isiyotarajiwa na kila mtu kama ambavyo mwizi huja. Anga itatoweka kwa muungurumo wa sauti kuu. Kila kitu kilicho angani kitateketezwa kwa moto. Na dunia na kila kitu kilichofanyika ndani yake kitafunuliwa na kuhukumiwa na Mungu. Kila kitu kitateketezwa kwa namna hii. Sasa mnapaswa kuishi kwa namna gani? Maisha yenu yanapaswa kuwa matakatifu na yanayompa heshima Mungu. Mnapaswa kuangalia mbele, kuiangalia siku ile ya Bwana, mkifanya kile mnachoweza ili ije mapema. Itakapofika, anga itateketezwa kwa moto na kila kitu kilicho angani kitayeyuka kwa joto. Lakini Mungu alituahidi. Na tunasubiri alichoahidi, yaani anga mpya na dunia mpya. Mahali ambapo hakia unaishi. Rafiki wapendwa, tunasubiri hili litokee. Hivyo jitahidini kadri mnavyoweza msiwe na dhambi wala kosa. Jitahidini kuwa na amani na Mungu. Kumbukeni kuwa tumeokolewa kwa sababu Bwana wetu ni mvumilivu. Ndugu yetu mpendwa Paulo aliwaambia jambo hili hili alipowaandikia kwa hekima aliyopewa na Mungu. Ndivyo anavyosema katika barua zake zote anapoandika kuhusu mambo haya. Sehemu zingine katika barua zake ni ngumu kuzielewa, na kuna baadhi ya watu huzifafanua vibaya. Watu hawa ni wajinga na wasioaminika. Watu hawa hutoa pia maana potofu kwa Maandiko mengine. Lakini kwa kufanya hivi wanajiangamiza wao wenyewe. Rafiki wapendwa, tayari mnajua kuhusu hili. Hivyo iweni waangalifu. Msiwaruhusu watu hawa waovu wakawaongoza kwenye upotevu kwa mabaya wanayofanya. Jichungeni msipoteze imani yenu iliyo imara. Lakini mkue katika neema na kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu ni wake, sasa na hata milele! Amina. Tunataka tuwaambie juu ya Neno linalo toa uzima. Yeye aliyekuwepo tangu mwanzo. Huyu ndiye yule tuliyemsikia na kumwona kwa macho yetu. Tuliyaona mambo aliyeyafanya, na mikono yetu ilimgusa. Ndiyo, yeye aliye uzima alidhihirishwa kwetu. Tulimwona, na hivyo tunaweza kuwaeleza wengine juu yake. Sasa tunawaeleza habari kwamba yeye ndiye uzima wa milele aliyekuwa pamoja na Mungu Baba na alidhihirishwa kwetu. Tuna wasimulia mambo tuliyoyaona na kuyasikia kwa sababu tunawataka muwe na ushirika pamoja nasi. Ushirika tulionao ni pamoja na Mungu Baba na mwanaye Yesu Kristo. Tunawaandikia mambo haya ili furaha yetu iwe kamili. Tulisikia mafundisho ya kweli toka kwa Mungu. Na sasa tunayasimulia kwenu. Mungu ni nuru, na ndani yake hamna giza. Kwa hiyo kama tukisema kuwa tunashirikiana na Mungu, lakini tukaendelea kuishi katika giza, tunakuwa ni waongo, tusioifuata kweli. Tunapaswa kuishi katika nuru, ambamo Mungu yupo. Kama tunaishi katika nuru, tunashirikiana sisi kwa sisi, na sadaka ya damu yake Yesu, Mwana wa Mungu, inatutakasa kila dhambi. Kama tukisema kuwa hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na tumeikataa kweli. Lakini kama tukiungama dhambi zetu, Mungu atatusamehe. Tunaweza kumwamini Mungu kufanya hili. Kwa sababu Mungu daima hufanya lililo haki. Atatufanya tuwe safi toka kila dhambi tuliyofanya. Kama tukisema kuwa hatujafanya dhambi, tunasema kuwa Mungu ni mwongo na tumeyakana mafundisho yake. Wapendwa wanangu, ninawaandikieni waraka huu ili kwamba msitende dhambi. Ila kama yeyote akitenda dhambi, tunaye Yesu Kristo wa kutusaidia. Yeye daima alitenda haki, kwa hiyo anaweza kututetea mbele za Mungu Baba. Yesu ndiye njia ambapo dhambi zetu zinaondolewa. Naye haziondoi dhambi zetu tu bali anaziondoa dhambi za watu wote. Kama tukitii mambo ambayo Mungu ametuamuru kuyafanya, tunapata uhakika ya kuwa tunamjua. Kama tukisema kuwa tunamjua Mungu lakini hatuzitii amri zake, tunasema uongo. Kweli haimo ndani mwetu. Lakini tunapotii mafundisho ya Mungu, kwa hakika upendo wake unakamilika ndani yetu. Hivyo ndivyo tunavyojua kuwa tunaishi ndani yake. Kama tukisema kuwa tunaishi ndani ya Mungu, ni lazima tuishi kwa namna ambvyo Yesu aliishi. Wapendwa rafiki zangu, siwaandiki ninyi amri mpya. Ni amri ile ile ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ni fundisho lile lile ambalo mmekwishalisikia. Lakini kile ninachokiandika pia ni amri mpya. Ni kweli; Mnaweza kuiona kweli ndani ya Yesu na ndani yenu ninyi wenyewe. Giza linatoweka, na nuru ya kweli tayari inang'aa. Mtu anaweza kusema, “Niko nuruni,” lakini ikiwa anamchukia ndugu yeyote katika familia ya Mungu, basi angali bado katika giza. Wao wanaowapenda ndugu wanaishi katika nuru, na hakuna kitu ndani yao cha kuwafanya watende mabaya. Lakini yeyote anayemchukia nduguye wa kike au wa kiume yuko gizani. Anaishi katika giza. Hajui anakoenda, kwa sababu giza limemfanya asiweze kuona. Ninawaandikia, ninyi watoto wapendwa, kwa sababu dhambi zenu zimesamehewa kwa njia ya Kristo. Ninawaandikia, ninyi akina baba, kwa sababu mnamjua yeye aliyekuwepo tangu mwanzo. Ninawaandikia, ninyi vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Ninawaandikia ninyi watoto, kwa sababu mnamjua Baba. Ninawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mnamfahamu yeye aliyekuwepo tangu mwanzo. Ninawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu. Mafundisho ya Neno la Mungu yimo ndani yenu, na mmemshinda yule mwovu. Msiipende dunia hii ya uovu wala mambo yaliyomo ndani yake. Kama mkiipenda dunia, upendo wa baba haumo ndani yenu. Yote yaliyomo katika dunia: yaani, tamaa halisi za kibinadamu, tamaa kwa yale mabaya tunayoyaona, na kiburi cha vitu tulivyonavyo. Lakini hakuna hata mojawapo ya haya litokalo kwa Baba. Yote yanatoka katika dunia. Dunia inapita, na mambo yote ambayo watu wanayataka kutoka katika dunia nayo yanapita. Lakini yeyote atendaye mambo ambayo Mungu anayataka ataishi milele. Wapendwa wanangu, mwisho umekaribia! Mmesikia kuwa adui wa Kristo anakuja. Na sasa maadui wengi wa Kristo tayari wapo hapa. Hivyo tunajua kwamba mwisho umekaribia. Maadui hawa walikuwa miongoni mwetu, lakini walituacha. Hawakuwa wenzetu hasa. Kama wangelikuwa kweli wenzetu, wangebaki pamoja nasi. Lakini walituacha. Hii inaonesha kuwa hakuna hata mmoja wao aliyekuwa kwa hakika mwenzetu. Mnayo karama aliyowapa Yeye Aliye Mtakatifu. Hivyo nyote mnaijua kweli. Mnadhani ninawaandikia waraka huu kwa sababu hamuijui kweli? Hapana! Ninawaandikia kwa sababu mnaijua kweli. Na mnajua kuwa hakuna uongo utokao katika kweli. Ni nani basi aliye mwongo? Ni yeye anayesema kuwa Yesu siyo Kristo. Yeyote anayesema hivyo ni adui wa Kristo. Yeye huyo asiyemwamini Baba wala Mwana. Yeyote asiyemwamini Mwana hana Baba, ila yeye anayemkubali Mwana anaye Baba pia. Mnapaswa kuendelea kuyafuata mafundisho mliyoyasikia tangu mwanzo. Kama mkifanya hivyo, mtakuwa siku zote katika Mwana na katika Baba. Na hili ndilo ambalo Mwana ameliahidi kwetu sisi, uzima wa milele. Ninawaandikia barua hii juu ya wale ambao wanataka kuwapotosha katika njia isiyo sahihi. Kristo aliwapa karama maalumu. Nanyi bado mngali na karama hiyo ndani yenu. Hivyo hamumhitaji yeyote kuwafundisha. Karama aliyowapa inawafundisha juu ya kila jambo. Ni karama ya kweli, si ya uongo. Hivyo endeleeni kuishi katika Kristo, kama karama yake ilivyowafundisha. Ndiyo, wanangu wapendwa, ishini ndani yake. Kama tukifanya hivyo, hatutakuwa na hofu siku kristo atakapo kuja tena. Hatutahitaji kujificha na kuwa na aibu ajapo. Mnajua ya kwamba daima Kristo alifanya yaliyo ya haki. Vivyo hivyo mnajua pia ya kwamba wote watendao haki ni watoto wa Mungu. Baba ametupenda sisi sana! Hili linaonesha jinsi anavyotupenda: Tunaitwa watoto wa Mungu. Ni kweli kuwa tu watoto wa Mungu. Lakini watu waliomo duniani hawaelewi ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu, kwa sababu hawamjui yeye. Wapendwa, sasa tu watoto wa Mungu. Mungu hajatuonyesha bado namna tutakavyokuwa wakati unaoukuja. Lakini tunajua ya kwamba Kristo atakapokuja tena, tutafanana naye. Tutamwona kama alivyo. Ni mtakatifu, na kila aliye na matumaini haya katika yeye huendelea kuwa mtakatifu. Kila atendaye dhambi huivunja sheria ya Mungu. Ndiyo, kutenda dhambi ni sawa na kuishi kinyume na sheria ya Mungu. Mwajua ya kuwa Kristo alikuja kuziondoa dhambi za watu. Haimo dhambi ndani ya Kristo. Hivyo kila anayeishi katika Kristo haendelei kutenda dhambi. Kama wakiendelea kutenda dhambi, kwa hakika hawajamwelewa Kristo na hawajamjua kamwe. Watoto wapendwa, msimruhusu mtu yeyote kuwadanganya. Kristo daima alitenda yaliyo haki. Hivyo kuwa mwema kama Kristo, ni lazima utende yaliyo haki. Mwovu amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kila anayeendelea kutenda dhambi ni mali ya Mwovu. Mwana wa Mungu alikuja kwa ajili ya hili: Kuziharibu kazi za Mwovu. Wale ambao ni watoto wa Mungu hawaendelei kutenda dhambi, kwa sababu wanayo maisha mapya waliyopewa na Mungu. Hawaendelei kutenda dhambi, kwa sababu wamefanyika watoto wa Mungu. Hivyo tunaweza kuwatambua walio watoto wa Mungu na walio watoto wa Mwovu. Hawa ndiyo wasio watoto wa Mungu: Wale wanaotenda mambo yasiyo haki na wale wasiowapenda ndugu zao wa kike na wa kiume katika familia ya Mungu. Haya ni mafundisho mliyoyasikia toka mwanzo: Ni lazima tupendane sisi kwa sisi. Msiwe kama Kaini. Aliyekuwa upande wa Mwovu. Kaini alimwua ndugu yake. Lakini kwa nini alimwua? Ni kwa sababu alichokifanya Kaini kilikuwa cha kiovu, na alichokifanya nduguye kilikuwa cha haki. Kaka zangu na dada zangu, msishangae watu wa dunia hii wakiwachukia. Tunafahamu ya kuwa tumevuka kutoka mautini na kuingia uzimani. Tunafahamu hili kwa sababu tunapendana sisi kwa sisi kama ndugu wa kike na wa kiume. Yeyote asiyewapenda kaka zake na dada zake angali amekufa. Kila anayemchukia nduguye anayeamini ni muuaji. Nanyi mnajua kuwa hakuna muuaji aliye na uzima wa milele. Hivi ndivyo tunavyojua jinsi upendo wa kweli ulivyo: Yesu aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Hivyo nasi tunapaswa kuyatoa maisha yetu, kwa ajili ya ndugu wa kike na wa kiume katika familia ya Kristo. Itakuwaje pale muumini tajiri mwenye fedha za kutosha kupata mahitaji yake yote akamwona dada ama kaka yake aliye maskini na asiye na fedha za kutosha kupata mahitaji yake yote. Endapo muumini huyu tajiri hatamsaidia muumini yule maskini, basi ni wazi kwamba upendo wa Mungu haumo ndani ya muumini yule tajiri. Watoto wangu, upendo wetu usiwe wa maneno na kuongea tu. Hapana, upendo wetu unapaswa kuwa halisi. Hatuna budi kuuonyesha upendo wetu kwa mambo yale tunayofanya. Hivyo ndivyo tunavyojua kuwa sisi tu wa ile njia ya kweli. Pale mioyo yetu inapotufanya tujisikie kuwa na hatia, bado tunaweza kuwa na amani mbele za Mungu, kwa sababu Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu. Yeye anajua kila kitu. *** Rafiki zangu wapendwa, ikiwa hatujisikii kuwa tunatenda yasiyo haki, basi hatupaswi kuwa na hofu tunapoenda kwa Mungu. Na Mungu anatupa kile tunachomwomba. Nasi tunapokea kwa sababu tunazitii amri za Mungu na kufanya yanayompendeza. Hili ndilo Mungu analoliamuru: Kwamba tumwamini Mwanaye Yesu Kristo, na kwamba tupendane sisi kwa sisi kama alivyoamuru. Wote wanaozitii amri za Mungu wanaishi ndani ya Mungu. Na Mungu anaishi ndani yao. Tunajuaje kuwa Mungu anaishi ndani yetu? Tunajua kwa sababu ya Roho aliyetupa sisi. Rafiki zangu wapenzi, manabii wengi wa uongo wapo duniani sasa. Hivyo msiiamini kila roho, lakini zijaribuni hizo roho ili muone kama zinatoka kwa Mungu. Hivi ndivyo mwezavyo kuitambua Roho ya Mungu. Roho inayosema, “Naamini kuwa Yesu ni Masihi aliye kuja duniani na akafanyika mwanadamu.” Roho hiyo inatoka kwa Mungu. Roho inayokataa kutamka hayo juu ya Yesu, hii ni roho iliyo adui kwa Kristo. Mmesikia kuwa adui wa kristo anakuja, na sasa amekwishakuja naye yupo tayari ulimwenguni. Wanangu wapenzi, ninyi ni wa Mungu, hivyo mmeshawashinda tayari hawa manabii wa uongo. Hii ni kwa sababu yule aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliyeko duniani. Wao ni wa ulimwengu. Hivyo kile wanachokisema ni cha ulimwengu pia. Na ulimwengu husikia kile wanachokisema. Lakini sisi tunatokana na Mungu. Kwa hiyo watu wanaomjua Mungu hutusikia sisi. Lakini watu wasiotokana na Mungu hawatusikii sisi. Hivi ndivyo tunavyiojua Roho iliyo ya kweli na ile iliyo ya uongo. Wapenzi rafiki, tunatakiwa tupendane sisi kwa sisi, kwa sababu upendo watoka kwa Mungu. Yeyote apendae amefanyika mwana wa Mungu. Na kila apendae anamfahamu Mungu. Kila asiyependa hamfahamu Mungu, kwa sababu Mungu ni Pendo. Hivi ndivyo Mungu alivyo tuonyesha pendo lake sisi: Alimtuma mwanawe wa pekee ulimwenguni kutupatia sisi uzima katika yeye. Upendo wa kweli ni upendo wa Mungu kwa ajili yetu, si upendo wetu kwa Mungu. Alimtuma mwanawe kama njia ya kuziondoa dhambi zetu. Hivyo ndivyo Mungu atupendavyo, rafiki wapenzi! Kwa hiyo tupendane sisi kwa sisi. Hakuna aliyemwona Mungu. Ila tukipendana sisi kwa sisi, Mungu anaishi ndani yetu. Kama tukipendana sisi kwa sisi, Upendo wa Mungu unafikia shabaha yake na unafanywa kamili ndani yetu. Twatambua kuwa tunaishi katika Mungu na mungu ndani yetu. Twalitambua hilo kwa sababu ametupa Roho wake. Tumeona kuwa Baba alimtuma mwanaye aje kuwa Mwokozi wa ulimwengu, na hili ndilo tunalowaambia watu sasa. Yeyote anayesema, “Naamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu,” huyo ni mtu anayeishi ndani ya Mungu, na Mungu anaishi ndani ya mtu huyo. Hivyo twalifahamu pendo alilonalo Mungu kwetu, na tunalitumainia pendo hilo. Mungu ni pendo. Kila anae ishi katika pendo anaishi ndani ya Mungu, na Mungu ndani yao. Kama pendo la Mungu limekamilishwa ndani yetu, tunaweza kuwa bila hofu siku ambayo Mungu atahukumu ulimwengu. Hatutakuwa na hofu, kwa sababu katika ulimwengu huu tunaishi kama Yesu. Palipo na upendo wa Mungu, hakuna hofu, kwa sababu upendo wa Mungu ulio kamili unaondoa hofu. Ni hukumu yake ndiyo inayomfanya mtu kuwa na hofu. Hivyo pendo lake halikamilishwi kwa mtu ambaye ndani yake kuna hofu. Tunapenda kwa sababu Mungu alitupenda sisi kwanza. Kama tukisema kuwa tunampenda Mungu na tunamchukia mmojawapo wa kaka na dada zetu katika familia ya Mungu, basi sisi tu waongo. Kama hatuwezi kumpenda mtu tunayemwona, tutawezaje kumpenda Mungu, ambaye hata hatujamwona. Mungu ametupa amri hii: Kama tunampenda Mungu, Ni lazima pia tupendane sisi kwa sisi kama kina kaka na kina dada. Watu wanao amini kuwa Yesu ni Masihi ni wana wa Mungu. Na kila ampendae Baba pia anawapenda watoto wa Baba. Twatambuaje kuwa tunawapenda watoto wa Mungu? Twatambua kwa sababu tunampenda Mungu na tunazitii amri zake. Kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake. Na amri za Mungu si ngumu kwetu, kwa sababu kila ambae ni mwana wa Mungu ana uwezo wa kushinda dhidi ya ulimwengu. Ni imani yetu iliyoshinda vita dhidi ya ulimwengu. Hivyo ni nani anayeushinda ulimwengu? Ni wale tu wanaoamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu. Yesu Kristo ndiye aliyekuja. Alikuja kwa maji na damu. Hakuja kwa maji peke yake. Lahasha, Yesu alikuja kwa vyote maji na damu. Na Roho atuambia kuwa hili ni kweli. Roho ndiye Kweli. Kwa hiyo kuna mashahidi watatu wanao tuambia habari za Yesu: Roho, Maji, na Damu. Mashuhuda hawa watatu wanakubaliana. Tunawaamini watu wanaposema jambo llililo kweli. Lakini kile anachosema Mungu ni muhimu zaidi. Na Hivi ndivyo Mungu alivyotuambia: Alituambia ukweli kuhusu Mwanaye. Kila amwaminiye Mwana wa Mungu anayo kweli ambayo Mungu alituambia. Lakini watu wasiomwamini Mungu wanamfanya Mungu kuwa mwongo, kwa sababu hawaamini kile ambacho Mungu ametueleza kuhusu mwanaye. Hiki ndicho ambacho Mungu alitueleza: Mungu ametupatia uzima wa milele, na uzima huu umo katika wanawake. Yeyote aliye na mwana anao uzima wa milele, lakini asiye na mwana wa mungu hana huo uzima wa milele. Ninawaandikia barua hii ninyi mnaomwamini Mwana wa Mungu ili mjue ya kwamba sasa mnao uzima wa milele. Tunaweza kwenda kwa Mungu tukiwa na ujasiri huo. Hii ina maana kuwa tunapomwomba Mungu mambo (na mambo hayo yakakubaliana na matakwa yake kwetu), Mungu huyajali yale tunayosema. Hutusikiliza kila wakati tunapomwomba. Hivyo tunatambua kuwa yeye hutupa kila tunachomwomba. Utakapomwona muumini mwenzio akitenda dhambi (Dhambi isiyomwongoza kwenye mauti), unapaswa kumwombea. Kisha Mungu atampa uzima. Ipo aina ya dhambi inayomwongoza mtu hadi mauti ya milele. Sina maana ya kusema unapaswa kuombea aina hiyo ya dhambi. Daima kutenda yasiyo haki ni dhambi. Lakini ipo dhambi isiyomwongoza mtu katika mauti ya milele. Tunajua kwamba wale waliofanyika watoto wa Mungu hawaendelei kutenda dhambi. Mwana wa Mungu anawahifadhi salama. Yule Mwovu hawezi kuwagusa. Tunajua kwamba sisi ni wa Mungu, Lakini yule Mwovu anautawala ulimwengu wote. Nasi tunajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja na ametupa uelewa. Hivyo sasa tunaweza kumjua yeye aliye kweli, na tunaishi katika Mungu huyo wa kweli. Nasi tumo ndani ya mwanaye, Yesu Kristo. Yeye ndiye Mungu wa kweli, naye ndiye uzima wa milele. Kwa hiyo, watoto wapendwa, mjiepushe na miungu wa uongo. Salamu kutoka kwa mzee. Kwa mwanamke aliyechaguliwa na Mungu na kwa wanawe. Kweli kabisa, ninawapenda ninyi nyote. Na sio mimi peke yangu. Bali wote wanaoifahamu kweli wanawapenda vile vile. Tunawapenda kwa sababu ya kweli, ile kweli iliyomo ndani yetu. Kweli inayoendelea kuwemo ndani yetu milele yote. Neema, rehema, na amani itakuwa pamoja nasi kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa mwanaye, Yesu Kristo, kwa kadri tuishivyo katika kweli na upendo. Nilikuwa na furaha sana baada ya kufahamu habari za baadhi ya watoto wako. Nina furaha kuwa wanaifuata njia ya kweli, kama vile baba alivyo tuamuru. Na sasa, mwanamke mwema, nina ombi hili: na tupendane sisi kwa sisi. Hii si amri mpya. Ni amri ile ile tuliyo kuwa nayo tangu mwanzo. Na hii ndiyo maana ya kupenda: kuishi kulingana na amri zake. Na amri ya Mungu ni hii: Kwamba muishi maisha ya upendo. Mliisikia amri hii toka mwanzo. Walimu wengi wa uongo wamo duniani sasa. Wana kataa kusema Yesu ni Masihi aliyekuja duniani na kufanyika mwanadamu. Kila anayekataa kuikubali kweli hii ni mwalimu wa uongo na adui wa Kristo. Muwe waangalifu! Msiipoteze thawabu tuliyokwisha kuitendea kazi. Mhakikishe mnaipokea thawabu kamili. Kila mmoja aendelee kuyashika mafundisho aliyefundishwa juu Kristo tu. Yeyote atakayeyabadili mafundisho hayo hana Mungu. Kila anayeendelea kuyafuata mafundisho ya Kristo anao wote Baba na Mwanaye. Msiwakubali wale wanaowaijia lakini hawawaletei mafundisho haya. Msiwakaribishe katika nyumba zenu. Msiwape salamu zenu. Kama mkiwakaribisha na kuwasalimu, mnawasaidia katika kazi zao za uovu. Nina mengi ya kuwaambia. Lakini sitaki kutumia karatasi na wino. Badala yake, nataraji kuja kuwatembelea. Kisha tunaweza kujumuika pamoja na kuzungumza uso kwa uso. Ndipo furaha yetu itakamilika. Watoto wa dada yako aliyechaguliwa na Mungu wamekutumia upendo wao. Salamu toka kwa mzee. Kwa rafiki mpendwa gayo, mtu ni mpendae kwa dhati. Rafiki yangu mpendwa, najua kwamba unaendelea vizuri kiroho, kwa hiyo ninaomba kuwa mengine yote yaendelee vizuri pia nawe uwe na afya njema. Baadhi ya waamini walikuja na kunieleza juu ya kweli iliyo katika maisha yako. Waliniambia kuwa unaendelea kuifuata njia ya kweli. Hili lilinifanya nijisikie furaha sana. Daima hili hunipa furaha iliyo kuu ninaposikia kuwa wanangu wanaifuata njia ya kweli. Rafiki yangu mpendwa, inapendeza kuwa unaonesha uaminifu wako katika kazi yako yote miongoni mwa waaminio. Wengine ambao huwajui. Hao waliliambia kanisa juu ya upendo ulio nao. Tafadhali wasaidie kuendelea na safari yao. Wasaidie katika njia ambayo itampendeza Mungu. Safari hiyo waliyoenda ni ya kumtumikia Kristo. Hawakupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasioamini. Hivyo inatupasa kuwasaidia. Tunapowasaidia, tunashiriki kazi yao katika ile kweli. Niliandika barua kwa kanisa, ila Diotrefe hasikilizi yale tunayosema. Yeye daima anataka kuwa kiongozi. Nitakapokuja, nitaongea naye mbele ya kanisa juu ya hiki anachokifanya. Anadanganya na kusema mambo mabaya juu yetu, lakini hayo siyo yote. Anakataa kuwapokea na kuwasaidia wanaoamini wanaosafiri kwenda huko. Na hawaruhusu watu wengine kuwasaidia. Kama wakifanya hivyo, anawazuia wasikusanyike na kanisa tena. Rafiki yangu mpendwa, usiige lililo baya; bali iga lililo jema. Yeyote anayetenda yaliyo mema hutoka kwa Mungu. Ila yeyote anayetenda maovu bado hajamjua Mungu. Kila mtu azungumza yaliyo mema juu ya Demetrio, na kweli inakubaliana na yale wasemayo. Pia, twasema mema juu yake. Na unafahamu kuwa tusemayo ni kweli. Nina mambo mengi nataka kukueleza. Lakini sipendi kutumia kalamu na wino. Natumaini kukutembelea hivi karibuni. Hapo tunaweza kukaa pamoja na kuongea uso kwa uso. Amani kwako. Rafiki walio pamoja nami hapa wakutumia upendo wao. Tafadhali wapatie upendo wetu kila rafiki waliopo huko. Salamu kutoka kwa Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo na ndugu yake Yakobo. Kwa wale waliochaguliwa na kupendwa na Mungu Baba na kulindwa ndani ya Yesu Kristo. Rehema, amani na upendo viwe pamoja nanyi zaidi na zaidi. Rafiki wapendwa, nilitaka sana kuwaandikia kuhusu wokovu tunaoshiriki pamoja. Lakini nimejisikia kuwa ni muhimu niwaandikie kuhusu kitu kingine: Ninataka kuwatia moyo kuipigania kwa nguvu imani ambayo Mungu aliwapa watakatifu wake. Mungu alitoa imani hii mara moja na ni nzuri wakati wote. Baadhi ya watu wamejiingiza kwa siri kwenye kundi lenu. Watu hawa wamekwisha kuhukumiwa kuwa wakosaji kwa sababu ya matendo yao. Zamani zilizopita manabii waliandika kuhusu watu hao. Wako kinyume na Mungu. Wameigeuza neema ya Mungu kujihalalishia kutenda chochote wanachotaka. Wanakataa kumtii Mkuu aliye peke yake, Bwana wetu Yesu Kristo. Ninataka kuwasaidia mkumbuke baadhi ya vitu mnavyovifahamu tayari: Kumbukeni kwamba Bwana aliwaokoa watu wake kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. Na kumbukeni malaika waliopoteza mamlaka yao ya kutawala. Waliacha mahali pao pa kuishi. Hivyo Bwana amewaweka gizani, wamefungwa kwa minyororo ya milele, mpaka watakapohukumiwa siku iliyo kuu. Pia kumbukeni miji ya Sodoma na Gomora na miji mingine iliyoizunguka. Kama wale malaika, watu wa miji ile walikuwa na hatia ya dhambi ya uzinzi, hata wakataka kuzini na malaika. Na waliadhibiwa kwa moto wa milele. Miji hii ni mfano kwa waovu watakaoteseka kwa adhabu ya moto wa milele. Ni sawasawa na watu hawa waliojiingiza kwenye kundi lenu. Wanaongozwa na ndoto, wanajichafua wenyewe kwa dhambi. Wanapuuza mamlaka ya Bwana na kusema mambo mabaya kinyume na walio watukufu. Hata malaika mkuu Mikaeli hakufanya hivi. Mikaeli alibishana na Ibilisi kuhusu nani angeuchukua mwili wa Musa. Lakini Mikaeli hakutamka hukumu kwa Ibilisi kwa mashitaka yake ya uongo. Badala yake, Mikaeli alisema, “Bwana mwenyewe akuadhibu!” Lakini watu hawa hukashifu mambo wasiyoyaelewa. Wanaelewa baadhi ya mambo, isipokuwa wanayaelewa mambo haya si kwa kufikiri bali kwa kuhisi, kama wanyama wasiofikiri. Na haya ni mambo yanayowaangamiza. Itakuwa vibaya kwao kwa kuwa wameifuata njia ambayo Kaini aliitumia. Kwa kutafuta fedha, wamejiingiza katika kosa lile lile la Balaamu. Wamepigana kinyume na Mungu kama alivyofanya Kora. Na wataangamizwa vile vile kama Kora. Watu hawa ni kama madoa machafu miongoni mwenu, wanawatia aibu mnapokutanika pamoja kuonesha upendo miongoni mwenu na kula chakula kwa pamoja kama kanisa. Pasipo kuwa na aibu wanakula pamoja nanyi. Wanajijali wao wenyewe tu. Wao ni kama mawingu yasiyo na mvua yanayosukumwa na upepo kila upande. Wako kama miti isiyo na matunda wakati wa mavuno ambayo hung'olewa kutoka ardhini. Hivyo wamekufa mara mbili. Kama mapovu machafu juu ya mawimbi ya bahari, kila mtu anaweza kuona mambo ya aibu wanayoyafanya. Ni kama nyota zinazotangatanga angani. Nao wameandaliwa mahali penye giza kuu milele. Henoko, mtu wa kizazi cha saba kutoka Adamu, alisema hivi kuhusu watu hawa: “Tazama! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika watakatifu. Kumhukumu kila mmoja. Atawaadhibu wale wote walio kinyume naye kutokana na maovu waliyotenda kwa sababu ya kutokumheshimu. Ndiyo, Bwana atawaadhibu watenda dhambi wote hawa wasiomheshimu. Atawaadhibu kwa sababu ya mambo maovu waliyosema kinyume naye.” Watu hawa daima hulalamika na kutafuta ubaya kwa wengine. Daima hutenda mambo maovu wanayotaka kufanya. Hujisifu wenyewe. Huwatendea vyema baadhi ya watu kuliko wengine ili wapate vitu wanavyovitaka. Rafiki wapendwa, kumbukeni mambo ambayo mitume wa Bwana Yesu Kristo walisema kuwa yatatokea. Walisema, “Katika nyakati za mwisho kutakuwa watu wanaomcheka Mungu na kufanya yale wanayotaka kufanya tu, mambo ambayo ni kinyume na Mungu.” Hawa ni watu wanaowagawa katika makundi. Si wa rohoni kwa sababu hawana Roho Mtakatifu. Lakini ninyi, rafiki wapendwa, itumieni imani yenu takatifu zaidi kusaidiana ninyi kwa ninyi ili muwe imara zaidi katika imani. Ombeni kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Jiwekeni salama katika upendo wa Mungu, kadri mnavyomsubiri Bwana Yesu Kristo kuionesha rehema yake kwenu kwa kuwapa uzima wa milele. Waonesheni rehema walio na mashaka. Waokoeni wale wanaoishi katika hatari ya moto wa jehanamu. Muwatendee wengine kwa rehema, lakini muwe waangalifu kuwa maisha yao maovu yasichafue mwenendo wenu mwema. Mungu ana nguvu na anaweza kuwafanya msianguke. Anaweza kuwaingiza katika uwepo wa utukufu wake bila makosa yoyote ndani yenu na akawapa furaha kuu. Ni Mungu peke yake, aliye Mwokozi wetu. Kwake uwepo utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kupitia Yesu Kristo kwa wakati uliopita, uliopo na milele. Amina. Huu ni ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa ili awaoneshe watumishi wake yale ambayo ni lazima yatokee muda mfupi ujao. Yesu Kristo alimtuma malaika wake ili amwonyeshe Yohana, mtumishi wake, ambaye amesema kila kitu alichokiona. Ni ukweli alioambiwa na Yesu Kristo; ni ujumbe kutoka kwa Mungu. Ana heri anayesoma maneno ya ujumbe huu kutoka kwa Mungu kwa kupaza sauti na wale wanaousikia ujumbe huu na kuyatendea kazi yaliyoandikwa ndani yake. Wakati uliosalia ni mfupi. Kutoka kwa Yohana, Kwenda kwa makanisa saba yaliyo katika Asia: Neema na amani ziwe kwenu kutoka kwake aliyepo, aliyekuwepo daima na anayekuja; na kutoka katika roho saba zilizoko mbele ya kiti chake cha enzi; na kutoka kwa Yesu Kristo aliye shahidi mwaminifu. Aliye wa kwanza miongoni mwa watakaofufuliwa kutoka kwa wafu na ndiye mtawala wa wafalme wote wa dunia. Yesu ndiye anayetupenda na ametuweka huru na dhambi zetu kwa sadaka ya damu yake. Ametufanya sisi kuwa ufalme wake na makuhani wanaomtumikia Mungu, Baba yake. Utukufu na nguvu viwe kwa Yesu milele na milele! Amina. Tazama, Yesu anakuja pamoja na mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma. Watu wote wa dunia watamwombolezea. Ndiyo, hili litatokea! Amina. Bwana Mungu asema, “Mimi ni Alfa na Omega. Mimi ndiye niliyepo, aliyekuwepo na anayekuja. Mimi ni Mwenye Uwezo Wote.” Mimi ni Yohana, mwamini mwenzenu. Tuko pamoja katika Yesu na tunashirikiana mambo haya: mateso, ufalme na uvumilivu wenye subira. Nilikuwa katika kisiwa cha Patmo kwa sababu nimekuwa mwaminifu kwa ujumbe wa Mungu na kwa ajili ya kweli ya Yesu. Siku ya Bwana, Roho Mtakatifu alinitawala. Nilisikia sauti kuu nyuma yangu iliyosikika kama tarumbeta. Ilisema, “Yaandike kwenye kitabu yale unayoyaona na uyatume kwa makanisa saba ya Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.” Niligeuka nyuma nimwone aliyekuwa anazungumza nami. Nilipogeuka, niliona vinara saba vya taa vya dhahabu. Nikamwona mmoja katikati ya vinara aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa vazi refu, na mshipi wa dhahabu uliofungwa kuzunguka kifua chake. Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe kama theluji. Macho yake yalikuwa kama miali ya moto. Miguu yake ilikuwa kama shaba ing'aayo inapochomwa katika tanuru. Sauti yake ilikuwa kama kelele za mafuriko ya maji. Alikuwa ameshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia. Upanga wenye makali kuwili ulitoka kinywani mwake. Uso wake ulikuwa jua linalong'aa sana mchana. Nilipomwona nilianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Aliweka mkono wake wa kulia juu yangu na kusema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa Mwisho. Mimi ndiye ninayeishi. Nilikufa, lakini tazama, niko hai milele na milele! Na ninashikilia funguo za mauti na Kuzimu. Hivyo andika unachokiona. Yaandike mambo yanayotokea sasa na mambo yatakayotokea baadaye. Hii ni maana iliyofichwa ya nyota na vinara saba vya taa vya dhahabu ulivyoviona: Vinara saba ni makanisa saba. Nyota saba ni malaika wa makanisa saba.” “Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso: Huu ni ujumbe kutoka kwake yeye anayeshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia na kutembea katikati ya vinara vya taa saba vya dhahabu. Ninayajua matendo yako, unavyofanya kazi kwa bidii na usivyokata tamaa. Ninajua kwamba huwakubali watu waovu. Umewajaribu wote wanaojiita mitume lakini si mitume. Umegundua kuwa ni waongo. Huachi kujaribu. Umestahimili taabu kwa ajili ya jina langu na hujakata tamaa. Lakini nina neno hili nawe umeuacha upendo uliokuwa nao hapo mwanzo. Hivyo kumbuka ulipokuwa kabla ya kuanguka. Ugeuze moyo wako na utende yale uliyoyatenda mwanzoni. Usipobadilika, nitakuja kwako na kutoa kinara chako cha taa mahali pake. Lakini unafanya vizuri kuyachukia matendo ya Wanikolai. Mimi pia nayachukia mambo wanayotenda. Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda, nitawapa haki ya kula matunda kutoka kwenye mti wa uzima, ulio katika Bustani ya Mungu. Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna: “Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa na akawa hai tena. Ninayajua matatizo yako, na ninajua kwamba wewe ni maskini, lakini hakika wewe ni tajiri! Ninayajua matusi unayoteseka kutoka kwa watu wanaojiita Wateule wa Mungu. Lakini si Wayahudi halisi. Watu hao ni wa kundi la Shetani. Usiogope mambo yatakayokupata hivi karibuni. Ninakwambia, Ibilisi atawafunga gerezani baadhi yenu ili kuipima imani yenu. Mtateseka kwa siku kumi, lakini iweni waaminifu, hata ikiwa mtatakiwa kufa. Mkiendelea kuwa waaminifu, nitawapa thawabu ya uzima wa milele. Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda hawatadhuriwa na mauti ya pili. Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo: Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye na upanga wenye makali kuwili unaotoka katika kinywa chake. Ninapafahamu mahali unapoishi. Unaishi mahali kilipo kiti cha enzi cha Shetani, lakini wewe ni mwaminifu kwangu. Hukukataa kueleza kuhusu imani yako kwangu hata wakati wa Antipa. Antipa alikuwa shahidi wangu mwaminifu aliyeuawa katika mji wako, mji ambao shetani anaishi. Lakini nina vitu vichache kinyume nawe. Una watu huko wanaofuata mafundisho ya Balaamu. Balaamu alimfundisha Balaki namna ya kuwafanya watu wa Israeli kutenda dhambi. Walitenda dhambi kwa kula vyakula vilivyotolewa kwa ajili ya sanamu na kwa kufanya uzinzi. Ndivyo ilivyo hata kwa kundi lako. Una watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai. Hivyo igeuzeni mioyo yenu! Msipobadilika, nitakuja kwenu haraka na kupigana kinyume na watu hawa kwa kutumia upanga unaotoka katika kinywa changu. Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa! Kila atakayeshinda nitampa mana iliyofichwa. Pia nitampa kila mshindi jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya juu yake. Na hakuna atakayejua jina hili isipokuwa yule atakayepata jiwe hili. Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira: Huu ni ujumbe kutoka kwa Mwana wa Mungu, aliye na macho yanayong'aa kama moto na miguu kama shaba inayong'aa. Ninayajua matendo yako. Ninajua kuhusu upendo wako, imani yako, huduma yako na uvumilivu wako. Ninajua kwamba unafanya zaidi sasa kuliko ulivyofanya kwanza. Lakini ninalo hili kinyume nawe: Umemruhusu yule mwanamke Yezebeli afanye anachotaka. Anasema kwamba yeye ni nabii, lakini anawapotosha watu wangu kwa mafundisho yake. Yezebeli huwaongoza watu wangu kutenda dhambi ya uzinzi na kula vyakula vilivyotolewa kwa sanamu. Nimempa muda ili aubadili moyo wake na kuiacha dhambi yake, lakini hataki kubadilika. Hivyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso. Na wale wote wanaozini naye watateseka sana. Nitafanya hivi sasa ikiwa hawataacha mambo anayofanya. Pia, nitawaua wafuasi wake. Ndipo makanisa yote wataona kuwa mimi ndiye ninayefahamu kile ambacho watu wanadhani na kufikiri. Na nitamlipa kila mmoja wenu kutokana na kile alichotenda. Lakini ninyi wengine mlioko Thiatira ambao hamjafuata mafundisho yake. Hamjajifunza mambo yanayoitwa ‘Siri za ndani za Shetani.’ Hivi ndivyo ninawaambia: Sitawatwika mzigo wowote. Shikeni katika kweli mliyo nayo tu mpaka nitakapo kuja. Nitawapa nguvu juu ya mataifa wale wote watakaoshinda na wakaendelea kutenda yale ninayotaka mpaka mwisho. Watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Watayavunja vipande vipande kama vyombo vya udongo wa mfinyanzi. Watakuwa na nguvu ile ile niliyoipokea kutoka kwa Baba yangu, na nitawapa nyota ya asubuhi. Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi: Huu ni ujumbe kutoka kwake Yeye mwenye roho saba na nyota saba. Ninayajua matendo yako. Watu husema kuwa u hai, lakini hakika umekufa. Amka! Jitie nguvu kabla ya nguvu kidogo uliyonayo haijakuishia kabisa. Unachofanya hakistahili kwa Mungu wangu. Hivyo usisahau kile ulichopokea na kusikia. Ukitii. Geuza moyo na maisha yako! Amka, la sivyo nitakuja kwako na kukushtukiza kama mwizi. Hautajua wakati nitakapokuja. Lakini una watu wachache katika kundi lako hapo Sardi waliojiweka safi. Watatembea pamoja nami. Watavaa nguo nyeupe, kwa kuwa wanastahili. Kila atakayeshinda atavikwa nguo nyeupe kama wao. Sitayafuta majina yao katika kitabu cha uzima. Nitawakiri mbele za Baba yangu na malaika zake ya kuwa wao ni wangu. Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia: Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye mtakatifu na wa kweli, anayeshikilia ufunguo wa Daudi. Anapofungua kitu, hakiwezi kufungwa. Na anapofunga kitu hakiwezi kufunguliwa. Ninayajua matendo yako. Nimeweka mbele yako mlango ulio wazi ambao hakuna anayeweza kuufunga. Ninajua wewe ni dhaifu, lakini umeyafuata mafundisho yangu. Hukuogopa kulisema jina langu. Sikiliza! Kuna kundi la Shetani. Wanasema kuwa wao ni Wayahudi, lakini ni waongo. Si Wayahudi halisi. Nitawafanya waje mbele yako na kusujudu kwenye miguu yako. Watajua ya kuwa ninakupenda. Umeifuata amri yangu kwa uvumilivu. Hivyo nitakulinda wakati wa shida itakayokuja ulimwenguni, wakati ambapo kila aishiye duniani atajaribiwa. Naja upesi. Ishikilie imani uliyonayo, ili mtu yeyote asiichukue taji yako. Wale watakaoshinda watakuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu. Hawataliacha hekalu la Mungu tena. Nitaandika juu yao jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu. Mji huo ni Yerusalemu mpya. Unateremka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Pia nitaandika jina langu jipya juu yao. Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia: Huu ni ujumbe kutoka kwa yeye aliye Amina, shahidi mwaminifu na wa kweli, aliye chanzo cha uumbaji wa Mungu. Ninayajua matendo yako. Wewe si moto wala baridi. Ninatamani kama ungekuwa moto au baridi! Lakini wewe ni vuguvugu tu, si moto, wala baridi. Hivyo niko tayari kukutema utoke mdomoni mwangu. Unasema wewe ni tajiri. Unadhani ya kuwa umekuwa tajiri na huhitaji kitu chochote. Lakini hujui kuwa wewe ni mnyonge, mwenye masikitiko, maskini, asiyeona na uko uchi. Ninakushauri ununue dhahabu kutoka kwangu, dhahabu iliyosafishwa katika moto. Kisha utakuwa tajiri. Nakuambia hili: Nunua kwangu mavazi meupe. Ndipo utaweza kuifunika aibu ya uchi wako. Ninakuagiza pia ununue kwangu dawa ya kuweka kwenye macho yako, nawe utaweza kuona. Mimi huwasahihisha na kuwaadhibu wale niwapendao. Hivyo onesha kuwa kuishi kwa haki ni muhimu kwako kuliko kitu kingine. Geuzeni mioyo na maisha yenu. Niko hapa! Nimesimama mlangoni nabisha hodi. Ikiwa utaisikia sauti yangu na ukaufungua mlango, nitaingia kwako na kula pamoja nawe. Nawe utakula pamoja nami. Nitamruhusu kila atakayeshinda kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi. Ilikuwa vivyo hivyo hata kwangu. Nilishinda na kuketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi. Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.” Kisha nikatazama, na mbele yangu ulikuwepo mlango uliokuwa wazi mbinguni. Na nikasikia sauti iliyosema nami mwanzoni. Ilikuwa sauti iliyosikika kama tarumbeta. Ilisema, “Njoo huku juu, nitakuonesha yale ambayo ni lazima yatokee baada ya hili.” Ghafla Roho akanichukua, na huko mbinguni kilikuwepo kiti cha enzi na mmoja amekaa juu yake. Aliyekikalia alikuwa mzuri kama mawe ya thamani, kama yaspi na karneli. Pande zote kuzunguka kiti cha enzi kulikuwa upinde wa mvua wenye rangi kama zumaridi. Vilikuwepo viti vingine vya enzi ishirini na nne kuzunguka kiti cha enzi vilivyokaliwa na wazee ishirini na nne. Wazee walikuwa wamevaa nguo nyeupe na taji za dhahabu vichwani mwao. Mianga na ngurumo za radi vilitoka katika kiti cha enzi. Mbele ya kiti cha enzi zilikuwepo taa saba zikiwaka, ambazo ndizo Roho saba za Mungu. Pia mbele ya kiti cha enzi kilikuwepo kitu kilichoonekana kama bahari ya kioo, iiliyo angavu sana. Mbele ya kiti cha enzi na kukizunguka pande zake zote walikuwepo viumbe wenye uhai wanne. Walikuwa na macho kila mahali. Kiumbe wa kwanza alikuwa kama simba. Wa pili alikuwa kama fahali. Wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu. Wa nne alikuwa kama tai anayeruka. Kila mmoja wa hawa wenye uhai wanne alikuwa na mabawa sita. Walikuwa na macho kila mahali, ndani na nje. Usiku na mchana hawaachi kusema: “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Bwana Mungu Mwenye nguvu zote. Daima amekuwepo, yupo na anakuja.” Wenye uhai hawa wanne walikuwa wanampa utukufu, heshima na shukrani yule anayekaa kwenye kiti cha enzi, anayeishi milele na milele. Na kila wakati walifanya hivyo, wazee ishirini na nne waliinama mbele ya yule anayekaa kwenye kiti cha enzi. Wanamwabudu anayeishi milele na milele. Wanaweka taji zao mbele ya kiti cha enzi na kusema: “Bwana wetu na Mungu! Unastahili kupokea utukufu, heshima na nguvu. Uliumba vitu vyote. Kila kinachoishi kiliumbwa kwa sababu ulitaka.” Kisha niliona kitabu katika mkono wa kulia wa aliyekaa kwenye kiti cha enzi. Kitabu hiki kilikuwa na maandishi pande zote na kilikuwa kimefungwa kwa mihuri saba. Na nikamwona malaika mwenye nguvu, aliyeita kwa sauti kubwa, “Ni nani anayestahili kuivunja mihuri na kukifungua kitabu?” Lakini hakukuwa yeyote mbinguni au duniani au chini ya dunia ambaye angeweza kukifungua kitabu na kutazama ndani yake. Nililia sana kwa sababu hakuwepo aliyestahili kukifungua kitabu na kuangalia ndani yake. Lakini mmoja wa wazee akaniambia, “Usilie! Simba kutoka kabila la Yuda ameshinda. Ni mzaliwa wa Daudi. Anaweza kukifungua kitabu na mihuri yake saba.” Kisha nikamwona Mwanakondoo amesimama katikati karibu na kiti cha enzi kilichozungukwa na viumbe wanne wenye uhai. Wazee pia walikuwa wamemzunguka Mwanakondoo aliyeonekana kama aliyeuawa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambayo ni roho saba za Mungu zilizotumwa ulimwenguni kote. Mwanakondoo alikuja na akakichukua kile kitabu kutoka katika mkono wa kulia wa yule aliyeketi kwenye kiti enzi. Baada ya Mwanakondoo kukichukua kile kitabu, viumbe wenye uhai wanne na wazee ishirini na wanne wakainama mbele za Mwanakondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi. Pia walikuwa wameshikilia bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni maombi ya watu watakatifu wa Mungu. Na wote walimwimbia wimbo mpya Mwanakondoo: “Unastahili kukichukua kitabu na kuifungua mihuri yake, kwa sababu uliuawa, na kwa sadaka ya damu yako uliwanunua watu kwa ajili ya Mungu, kutoka kila kabila, lugha, rangi na taifa. Uliwafanya kuwa ufalme na makuhani kwa ajili ya Mungu wetu. Nao watatawala duniani.” Kisha, nilipotazama, nikasikia sauti ya malaika wengi waliozunguka kiti cha enzi pamoja na viumbe wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne. Walikuwa maelfu kwa maelfu ya malaika, elfu kumi mara elfu kumi. Kwa sauti kuu malaika walisema: “Mamlaka yote, utajiri, hekima na nguvu ni kwa Mwanakondoo aliyeuawa. Anastahili kupokea heshima, utukufu na sifa!” Ndipo nikasikia kila kiumbe kilichoumbwa kilichoko mbinguni na duniani na chini ya dunia na baharini, viumbe vyote sehemu hizo vikisema: “Sifa zote na heshima na utukufu na nguvu kuu ni kwa ajili yake Yeye aketiye kwenye kiti cha enzi na kwa Mwanakondoo milele na milele!” Viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amina!” Na wazee wakainama chini wakasujudu. Kisha nilitazama Mwanakondoo alipokuwa anaufungua muhuri wa kwanza kati ya mihuri saba. Kisha nikasikia sauti ya mmoja wa viumbe wenye uhai wanne akisema kwa sauti kama ngurumo ya radi ikisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mweupe mbele yangu. Mwendesha farasi aliyekuwa amempanda farasi huyo alikuwa na upinde na alipewa taji. Alimwendesha farasi akatoka kwenda kumshinda adui na ili kupata ushindi. Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa pili, nilimsikia kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mwekundu akitokea. Aliyekuwa anamwendesha farasi huyu alipewa mamlaka ya kuondoa amani duniani ili watu wauane. Alipewa upanga mkubwa. Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa tatu. Nilisikia kiumbe mwenye uhai wa tatu akisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mweusi mbele yangu. Aliyekuwa anamwendesha farasi huyu alikuwa na mizani mkononi mwake. Kisha nilisikia kitu kilichosikika kama sauti ikitokea pale walipokuwa viumbe wenye uhai wanne. Kikisema, “Kilo moja ya ngano au kilo tatu ya shayiri itagharimu mshahara wote wa siku moja. Lakini usiharibu upatikanaji wa mafuta ya mzeituni na divai!” Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa nne nilisikia sauti ya kiumbe wa nne mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mwenye rangi ya kijivu. Aliyempanda alikuwa mauti na kuzimu ilikuwa inamfuata nyuma yake kwa karibu. Alipewa mamlaka juu ya robo ya dunia kuwaua watu kwa upanga, njaa, magonjwa na kwa wanyama wa porini waliomo duniani. Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa tano, niliziona baadhi ya roho za wale waliokuwa waaminifu kwa neno la Mungu na kweli waliyopokea zikiwa chini ya madhabahu. Roho hizi zilipiga kelele kwa sauti kuu zikisema, “Mtakatifu na Bwana wa kweli, ni lini utakapowahukumu watu wa dunia na kuwaadhibu kwa kutuua sisi?” Kisha kila mmoja wao alipewa kanzu ndefu nyeupe. Wakaambiwa wasubiri kwa muda mfupi kwani bado walikuwepo ndugu zao katika utumishi wa Kristo ambao ni lazima wauawe kama wao. Roho hizi ziliambiwa zisubiri mpaka mauaji yote yatakapokwisha. Kisha nilitazama wakati Mwanakondoo anaufungua muhuri wa sita. Kulitokea tetemeko kubwa la ardhi na jua likawa jeusi kama gunia jeusi na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. Nyota zikaanguka chini duniani kama mtini uangushavyo tini zake upepo unapovuma. Anga iligawanyika katikati na pande zote zikajiviringa kama kitabu. Na kila mlima na kisiwa kiliondolewa mahali pake. Kisha watu wote wa ulimwengu, wafalme, watawala, makamanda wa majeshi, matajiri, wenye mamlaka na nguvu, kila mtumwa na asiye mtumwa, walijificha katika mapango na nyuma ya miamba milimani. Waliiambia milima na miamba, “Tuangukieni. Tuficheni mbali na uso wa yule aketiye kwenye kiti cha enzi. Tuficheni dhidi ya hasira ya Mwanakondoo! Siku kubwa ya hasira yao imefika. Hakuna anayeweza kupingana nayo.” Baada ya hili kutokea, niliwaona malaika wanne wamesimama kwenye pembe nne za dunia wakiwa wamezishikilia pepo nne za dunia. Walikuwa wanazuia upepo kupuliza katika nchi au katika bahari au kwenye mti wowote. Kisha nikaona malaika mwingine akija akitokea upande wa mashariki. Malaika huyu alikuwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Malaika akawaita kwa sauti kuu malaika wale wanne. Malaika hawa wanne walikuwa malaika ambao Mungu amewapa mamlaka ya kuidhuru dunia na bahari. Malaika akawaambia, “Msiidhuru nchi au bahari au miti kabla hatujawawekea alama kwenye vipaji vya nyuso zao wale wanaomtumikia Mungu wetu.” Kisha nikasikia idadi ya watu wenye alama ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao. Walikuwa watu 144,000. Walitoka katika kila kabila la Israeli: Kutoka katika kabila la Yuda walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Rubeni walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Gadi walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Asheri walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Naftali walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Manasse walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Simeoni walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Lawi walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Isakari walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Zabuloni walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Yusufu walikuwa elfu kumi na mbili Kutoka katika kabila la Benjamini walikuwa elfu kumi na mbili. Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu. Walikuwa wengi hakuna mtu angeweza kuwahesabu wote. Walikuwa wametoka katika kila taifa, kabila, rangi za watu na lugha za dunia. Walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo. Wote walikuwa wamevaa majoho meupe na wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. Walipaza sauti kwa nguvu, wakasema “Ushindi ni wa Mungu wetu, anayeketi kwenye kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo.” Wazee na wenye uhai wanne walikuwa pale. Malaika wote walikuwa wamesimama kuwazunguka na kukizunguka kiti cha enzi. Malaika wakainamisha nyuso zao, wakasujudu mpaka chini mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu. Walisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, nguvu na uweza ni vyake Mungu wetu milele na milele. Amina!” Kisha mmoja wa wazee akaniuliza, “Watu hawa waliovaa kanzu nyeupe ni akina nani? Wametoka wapi?” Nikajibu, “Wewe unajua ni akina nani, bwana.” Mzee akasema, “Hawa ni wale waliokuja kutokana na mateso makuu. Wamefua kanzu zao kwa kutumia damu ya Mwanakondoo, wako safi na ni weupe. Hivyo sasa watu hawa wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Wanamwabudu Mungu mchana na usiku hekaluni mwake. Naye aketiye kwenye kiti cha enzi atawalinda. Hawatasikia njaa tena. Hawatasikia kiu tena. Jua halitawadhuru. Hakuna joto litakalowachoma. Mwanakondoo mbele ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao. Atawaongoza kwenda kwenye chemichemi za maji ya uzima. Na Mungu atafuta kila chozi kutoka kwenye macho yao.” Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa saba, kulikuwa ukimya mbinguni kama nusu saa hivi. Niliwaona malaika saba wanaosimama mbele ya Mungu. Walipewa tarumbeta saba. Malaika mwingine akaja na kusimama kwenye madhabahu. Malaika huyu alikuwa na chetezo ya dhahabu. Malaika alipewa ubani mwingi ili autoe pamoja na maombi ya watakatifu wote wa Mungu. Malaika akaweka sadaka hii juu ya madhabahu ya dhahabu mbele ya kiti cha enzi. Moshi kutoka kwenye ubani ukatoka kwenye mikono ya malaika kwenda kwa Mungu. Moshi ukaenda kwa Mungu ukiwa na Maombi ya watakatifu. Kisha malaika akaijaza chetezo moto kutoka madhabahuni na kuitupa chini duniani, kukatokea miali, radi na ngurumo zingine na tetemeko la ardhi. Kisha malaika saba wenye tarumbeta walijiandaa kupuliza tarumbeta zao. Malaika wa kwanza alipuliza tarumbeta yake. Mvua ya mawe na moto uliochanyanyikana na damu vilimwagwa chini duniani. Theluthi moja ya dunia na nyasi zote za kijani na theluthi ya miti vikaungua. Malaika wa pili alipopuliza tarumbeta yake. Kitu fulani kilichoonekana kama mlima mkubwa unaowaka moto kilitupwa baharini. Na theluthi moja ya bahari ikawa damu. Na theluthi moja ya viumbe walioumbwa wanaokaa baharini wakafa na ya meli theluthi moja zikaharibika. Malaika wa tatu alipopuliza tarumbeta yake. Nyota kubwa, inayowaka kama tochi ikaanguka kutoka mbinguni. Ilianguka kwenye theluthi moja ya mito na chemichemi za maji. Jina la nyota hiyo lilikuwa Uchungu. Na theluthi moja ya maji yote yakawa machungu. Watu wengi wakafa kutokana na kunywa maji haya machungu. Malaika wa nne alipopuliza tarumbeta yake. Theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota vikapigwa. Hivyo theluthi moja yao vikawa giza. Theluthi moja ya mchana na usiku ikakosa mwanga. Nilipokuwa ninatazama, nilimsikia tai aliyekuwa anaruka juu sana angani akisema kwa sauti kuu, “Ole! Ole! Ole kwa wale wanaoishi duniani! Shida kuu zitaanza baada ya sauti za tarumbeta ambazo malaika wengine watatu watapuliza.” Malaika wa tano alipopuliza tarumbeta yake, niliiona nyota ikianguka kutoka angani mpaka duniani. Nyota ilipewa ufunguo wa kufungulia shimo refu sana liendalo kuzimu. Kisha nyota ikafungua shimo refu sana liendalo kuzimu. Moshi ukatoka kwenye shimo kama moto utokao kwenye tanuru kubwa. Jua na anga vikawa giza kwa sababu ya moshi uliotoka kwenye shimo. Nzige wakatoka kwenye moshi na wakateremka kwenda duniani. Walipewa nguvu ya kuuma kama nge. Waliamriwa kutoharibu nyasi au mimea ya mashambani na mti. Walitakiwa kuwadhuru watu wasio na alama ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao tu. Hawakupewa mamlaka ya kuwaua lakini kuwatia maumivu kwa muda wa miezi mitano, maumivu kama ambayo mtu huyasikia anapoumwa na nge. Siku hizo watu watatafuta kifo, lakini hawatakiona. Watataka kufa, lakini kifo kitajificha. Nzige hao walionekana kama farasi walioandaliwa kwa ajili ya mapigano. Vichwani mwao walivaa kitu kilichoonekana kama taji ya dhahabu. Nyuso zao zilionekana kama nyuso za wanadamu. Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake. Meno yao yalikuwa kama meno ya simba. Vifua vyao vilionekana kama ngao za chuma. Sauti zilizotoka katika mbawa zao zilikuwa kama za farasi wengi na magari ya farasi yaendayo vitani. Walikuwa na mikia kama ya nge. Nguvu ya kuwasababishia wanadamu maumivu kwa miezi mitano ilikuwa kwenye mikia yao. Walikuwa na mtawala, aliyekuwa malaika wa kuzimu. Jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni. Na kwa Kiyunani ni Apolioni. Kitisho cha kwanza kimepita sasa. Bado vinakuja vitisho vingine viwili. Malaika wa sita alipopuliza tarumbeta yake, nilisikia sauti ikitoka katika pembe zilizo katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu. Ikamwambia malaika wa sita aliyekuwa na tarumbeta, “Wafungue huru malaika wanne waliofungwa pembezoni mwa mto mkuu Frati.” Malaika hawa wanne walikuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hii, siku hii, mwezi na mwaka huu. Malaika waliachwa huru ili waue theluthi moja ya watu duniani. Nikasikia kuwa idadi ya askari waliowaendesha farasi walikuwa milioni mia mbili. Katika maono yangu, niliona farasi na waendesha farasi wakiwa juu ya farasi. Walionekana hivi: Walivaa dirii za chuma vifuani mwao zilizokuwa za rangi nyekundu, rangi ya bahari iliyoiva na za rangi ya njano kama baruti. Vichwa vya farasi vilionekana kama vichwa vya simba. Farasi walikuwa wanatoa moto, moshi na baruti katika vinywa vyao. Theluthi ya watu wote duniani walikufa kutokana na mapigo haya matatu yaliyokuwa yanatoka vinywani mwa farasi: moto, moshi na baruti. Nguvu ya farasi ilikuwa kwenye midomo na mikia yao. Mikia yao ilikuwa kama nyoka walio na vichwa vya kuwauma na kuwadhuru watu. Watu wengine duniani hawakufa kwa mapigo haya. Lakini watu hawa bado hawakubadili mioyo yao na kuacha kuabudu vitu walivyovitengeneza kwa mikono yao wenyewe. Hawakuacha kuabudu mapepo na sanamu zilizotengenezwa kwa dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, au kusikia au kutembea. Hawakubadili mioyo yao na kuacha kuua watu wengine au kuacha uchawi, dhambi ya uzinzi na wizi. Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni akiwa amevikwa wingu na upinde wa mvua ulizunguka kichwa chake. Uso wake ulikuwa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto. Malaika alikuwa ameshika kitabu kidogo kilichofunguliwa. Akaweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na mguu wa kushoto nchi kavu. Alipaza sauti yake kama simba anavyounguruma na sauti za radi saba zikasikika. Radi saba ziliongea, na nikaanza kuandika. Lakini nilisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Usiandike ambacho radi saba zinasema. Yaache mambo hayo yawe siri.” Kisha nikamwona malaika aliyesimama juu ya bahari na nchi kavu akinyoosha mkono wake kuelekea mbinguni. Malaika akaapa kwa nguvu ya yule aishiye milele na milele. Ndiye aliyeziumba mbingu na vyote vilivyomo ndani yake. Aliumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, na aliumba bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Malaika alisema, “Hakutakuwa kusubiri tena! Katika siku ambazo malaika wa saba atakuwa tayari kupuliza tarumbeta yake, mpango wa siri wa Mungu utakamilika, nao ni Habari Njema ambayo Mungu aliwaambia watumishi wake, manabii.” Kisha nikasikia tena sauti ile ile kutoka mbinguni. Ikaniambia, “Nenda ukachukue kitabu kilicho wazi mkononi mwa malaika, aliyesimama juu ya bahari na nchi kavu.” Hivyo nilimwendea malaika nikamwomba anipe kitabu kidogo. Naye aliniambia, “Chukua kitabu na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako lakini kitakuwa kitamu kama asali mdomoni mwako.” Hivyo nilichukua kitabu kidogo kutoka mkononi mwa malaika na kukila. Mdomoni mwangu kilikuwa na ladha tamu kama asali, lakini baada ya kukila, kilikuwa kichungu tumboni mwangu. Kisha nikaambiwa, “Ni lazima uwatabirie tena watu wa asili tofauti, mataifa, lugha na watawala.” Kisha nilipewa fimbo ya kupimia, ndefu kama fimbo ya kutembelea. Nikaambiwa, “Nenda ukalipime hekalu la Mungu na madhabahu na uwahesabu watu wanaoabudu humo. Lakini usipime eneo lililo nje ya hekalu. Liache. Eneo hilo wamepewa watu wasio wa Mungu. Wataonesha nguvu zao juu ya mji mtakatifu kwa miezi 42. Nami nitawapa nguvu mashahidi wangu wawili, watatabiri kwa siku 1,260. Nao watakuwa wamevaa magunia.” Mashahidi hawa wawili ni mizeituni miwili na vinara viwili vya taa vinavyosimama mbele za Bwana wa dunia. Ikiwa mtu yeyote atajaribu kuwadhuru mashahidi hawa, moto utatoka katika vinywa vyao na kuwaua adui zao. Yeyote atakaye jaribu kuwadhuru atakufa. Mashahidi hawa wana nguvu ya kuzuia mvua isinyeshe katika wakati ambao watakuwa wanatabiri. Pia wana uwezo wa kugeuza maji kuwa damu. Wana uwezo wa kutuma kila aina ya pigo duniani. Wanaweza kufanya hivi kadri wanavyotaka. Mashahidi wawili watakapomaliza kuutangaza ujumbe wao, mnyama atokaye kuzimu atapigana nao. Atawashinda na kuwaua. Miili ya mashahidi hawa wawili italala kwenye mtaa wa mji mkuu. Mji huu unaitwa Sodoma na Misri. Majina ya mji huu yana maana maalumu. Huu ni mji ambako Bwana aliuawa. Watu kutoka kila asili, kabila, lugha na taifa wataiangalia miili ya mashahidi hawa wawili kwa siku tatu na nusu. Watu watakataa kuwazika. Na Kila aishiye duniani atafurahi kwa sababu mashahidi hawa wawili wamekufa. Watu watafanya sherehe na kupeana zawadi kwa sababu manabii hawa wawili walileta mateso mengi kwa watu waishio duniani. Lakini baada ya siku tatu na nusu, Mungu akawarudishia uhai mashahidi hawa wawili. Wakasimama kwa miguu yao. Na wale waliowaona wakajaa hofu. Kisha mashahidi wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikisema, “Njooni huku juu!” Na wote wawili wakaenda juu mbinguni katika wingu, adui zao wakiangalia wanavyokwenda. Katika wakati huo huo kulitokea tetemeko kuu la ardhi. Sehemu ya kumi ya mji ikateketea, na watu elfu saba wakafa. Wale ambao hawakufa waliogopa sana. Wakampa utukufu Mungu wa mbinguni. Kitisho cha pili kimepita. Kitisho cha tatu kinakuja haraka. Malaika wa saba alipopuliza tarumbeta yake, zikatokea sauti kuu mbinguni, zikasema: “Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Masihi wake sasa. Na atatawala milele na milele.” Kisha wazee 24 wakaanguka chini nyuso zao zikiwa chini wakamwabudu Mungu. Hawa ni wazee ambao wanakaa kwenye viti vyao vya heshima mbele za Mungu. Wazee wakasema: “Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi. Wewe ndiye uliyepo na ambaye daima umekuwepo. Tunakushukuru kwa sababu umetumia uweza wako mkuu na umeanza kutawala. Mataifa walikasirika, lakini sasa ni wakati kwa ajili ya hasira yako. Sasa ni wakati wa waliokufa kuhukumiwa. Ni wakati wa kuwapa thawabu watumishi wako, manabii, na kuwapa thawabu watu wako watakatifu, wakubwa na wadogo, wanaokuheshimu wewe. Ni wakati wa kuwaangamiza watu wanaoiangamiza dunia!” Kisha hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa. Sanduku la Agano likaonekana ndani ya hekalu lake. Kisha kukatokea miali ya radi na miungurumo ya radi, kelele, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe. Jambo la ajabu lilionekana mbinguni: Mwanamke aliyevalishwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake alionekana. Alikuwa na taji yenye nyota kumi na mbili kichwani pake. Alikuwa na mimba na alilia kwa uchungu kwa sababu alikuwa karibu ya kuzaa. Kisha ajabu nyingine ikaonekana mbinguni: Alikuweko huko joka mkubwa mwekundu. Joka huyo alikuwa na vichwa saba na alikuwa na taji juu ya kila kichwa. Na alikuwa na pembe kumi. Mkia wake ulizoa theluthi ya nyota na kuziangusha duniani. Joka hili lilisimama mbele ya mwanamke aliyekuwa karibu ya kuzaa mtoto. Lilitaka kumla mtoto mara atakapozaliwa. Mwanamke alimzaa mtoto wa kiume, atakayewatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya chuma. Na mwana wa mwanamke huyu alichukuliwa juu mbinguni kwa Mungu, kwenye kiti chake cha enzii. Mwanamke alikimbilia jangwani mpaka mahali ambako Mungu amemwandalia. Huko angetunzwa kwa siku 1,260. Kisha kulikuwa vita mbinguni. Mikaeli na malaika zake walipigana na joka. Nalo joka na malaika zake wakapigana na Mikaeli pamoja na malaika zake, lakini joka na malaika zake hawakuwa na nguvu za kutosha kushinda, na hivyo wakapoteza nafasi zao mbinguni. Likatupwa chini kutoka mbinguni. (Joka hili kubwa ni nyoka yule wa zamani, aitwaye Ibilisi au Shetani, anayeudanganya ulimwengu wote.) Joka na malaika zake walitupwa duniani. Kisha nilisikia sauti kubwa mbinguni ikisema: “Ushindi na uweza na ufalme wa Mungu wetu na mamlaka ya Masihi wake umekuja sasa, kwa sababu mshitaki wa kaka na dada zetu ametupwa chini. Ndiye aliyewashitaki kwa Mungu, mchana na usiku. Walimshinda kwa sadaka ya damu ya Mwanakondoo na kwa ujumbe wa Mungu waliowaambia watu. Hawakuyapenda maisha yao sana. Hawakuogopa kifo. Hivyo furahi, ewe mbingu na wote waishio humo! Lakini ole kwa nchi na bahari, kwa sababu Ibilisi ameshuka kwako. Amejaa ghadhabu. Anajua ana muda mchache.” Joka alipoona amekwisha tupwa chini duniani, alimkimbiza mwanamke aliyemzaa mtoto wa kiume. Lakini mwanamke alipewa mabawa mawili ya tai mkuu. Aliweza kuruka mpaka mahali palipoandaliwa kwa ajili yake jangwani. Huko atatunzwa kwa muda wa miaka mitatu na nusu akiwa mbali na joka. Kisha joka lilitoa maji kama mto kutoka katika kinywa chake kuelekea kwa mwanamke ili mafuriko yamchukue. Lakini nchi ilimsaidia mwanamke. Nchi ilifungua kichwa chake na kumeza mto uliotoka kwenye kinywa cha joka. Kisha joka lilimkasirikia sana mwanamke. Likaenda kufanya vita na watoto wake wengine. Watoto wa mwanamke ni wale wanaozitii amri za Mungu na wanayo kweli ambayo Yesu aliifundisha. Joka lilisimama ufukweni mwa bahari. Kisha niliona mnyama mwenye pembe kumi na vichwa saba akipanda kutoka baharini. Kila pembe yake ilikuwa na taji. Alikuwa na kumkufuru Mungu lililoandikwa kwenye kila kichwa. Mnyama huyu alionekana kama chui, miguu yake ilikuwa kama ya dubu. Mdomo wake ulikuwa kama wa simba. Joka akampa huyo mnyama uweza wake wote, kiti chake cha enzi na mamlaka kuu. Kichwa kimoja cha mnyama kilionekana kama kimejeruhiwa na kuuawa, lakini kidonda cha mauti kilipona. Watu wote ulimwenguni walishangaa, na wote walimfuata mnyama. Watu waliliabudu joka kwa sababu limempa nguvu mnyama, na pia walimwabudu mnyama. Waliuliza, “Nani ana nguvu kama mnyama? Nani anaweza kufanya vita dhidi yake?” Mnyama aliruhusiwa kujigamba na kumtukana Mungu na kutumia nguvu zake kwa miezi arobaini na mbili. Mnyama alifungua kinywa chake ili amtukane Mungu, alitukane jina lake, mahali anapoishi, na wale wote wanaoishi mbinguni. Alipewa uwezo wa kufanya vita na watakatifu wa Mungu na kuwashinda. Alipewa uwezo juu ya kila kabila, asili, lugha na taifa. Kila anayeishi duniani angemwabudu mnyama. Hawa ni watu wote ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo tangu mwanzo wa ulimwengu. Mwanakondoo ndiye yule aliyeuawa. Kila mtu anayesikia mambo haya azingatie hili: Yeyote ambaye ni lazima awe mfungwa, atakuwa mfungwa. Yeyote ambaye ni wa kuuawa kwa upanga, atauawa kwa upanga. Hii inamaanisha kwamba watakatifu wa Mungu lazima wawe na subira na imani. Pia nikaona mnyama mwingine akija kutoka katika nchi. Alikuwa na pembe mbili kama kondoo, lakini anaongea kama joka. Mnyama huyu alisimama mbele ya mnyama wa kwanza na kutumia nguvu ile ile ya mnyama wa kwanza. Alitumia nguvu hii kumfanya kila mtu aishiye duniani amwabudu mnyama wa kwanza. Mnyama wa kwanza ndiye mwenye jeraha la mauti lililopona. Mnyama wa pili alifanya miujiza mikuu. Alitengeneza hata moto ushuke kutoka mbinguni kuja duniani watu wakiangalia. Mnyama huyu wa pili aliwadanganya watu wanaoishi duniani kwa kutumia miujiza ambayo amepewa uwezo wa kuifanya kwa ajili ya mnyama wa kwanza. Aliwaamuru watu kutengeneza sanamu ili kumheshimu mnyama wa kwanza, aliyejeruhiwa kwa upanga lakini hakufa bali akawa hai tena. Mnyama wa pili alipewa uwezo wa kuipa uzima sanamu ya mnyama wa kwanza. Kisha kinyago kiliweza kuongea na kuamuru watu wote ambao hawakukiabudu wauawe. Pia mnyama wa pili aliwaamuru watu wote, wakubwa na wadogo, matajiri na maskini, walio huru au watumwa, wawekewe alama kwenye mikono yao ya kulia au kwenye vipaji vya nyuso zao. Hakuna ambaye angeweza kununua au kuuza bila ya kuwa na alama hii. (Alama hii ni jina la mnyama au namba ya jina lake.) Kila mwenye uelewa anaweza kujua maana ya namba ya mnyama. Hili linahitaji hekima. Namba hii ni namba ya mtu. Nayo ni 666. Kisha nikatazama, na mbele yangu alikuwepo Mwanakondoo, amesimama juu ya Mlima Sayuni. Watu 144,000 walikuwa pamoja naye. Jina lake na la Baba yake yalikuwa yameandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao. Nikasikia sauti kutoka mbinguni yenye kelele kama mafuriko au ngurumo ya radi. Lakini ilisikika kama sauti ya wapiga vinubi wapigao vinubi vyao. Watu waliimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na viumbe wenye uhai wanne na wazee. Walioujua wimbo mpya ni wale 144,000 tu walionunuliwa kutoka duniani. Hakuna mwingine tena aliyekuwa anaujua. Hawa ni wale ambao hawakuzini na wanawake. Walijiweka safi. Na Sasa wanamfuata Mwanakondoo kila aendako. Walinunuliwa kutoka miongoni mwa watu wa dunia ili kuwa wa kwanza, kuwa sadaka kwa Mungu na Mwanakondoo. Hawana hatia ya kusema uongo; hawana kosa. Kisha nikaona malaika mwingine akipaa juu angani, akitangaza Habari Njema ya milele kwa watu waishio duniani, watu wa kila taifa, kabila, lugha na rangi. Malaika akasema kwa sauti kuu, “Mcheni Mungu na msifuni yeye. Wakati wa Mungu kuwahukumu watu wote umefika. Mwabuduni Mungu. Aliumba mbingu, dunia, bahari na chemichemi za maji.” Kisha malaika wa pili akamfuata malaika wa kwanza na kusema, “Ameteketezwa! Mji mkuu Babeli umeteketezwa! Aliwafanya mataifa yote kunywa mvinyo wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu.” Malaika wa tatu aliwafuata malaika wawili wa kwanza. Malaika huyu wa tatu alisema kwa sauti kuu, “Mungu atawaadhibu wote wanaomwabudu mnyama na sanamu ya mnyama na kukubali kuwa na alama ya mnyama katika vipaji vya nyuso zao au kwenye mkono wao. Watakunywa mvinyo wa ghadhabu ya Mungu. Mvinyo huu umeandaliwa kwa nguvu zake zote katika kikombe cha ghadhabu ya Mungu. Watateseka kwa maumivu ya moto uwakao kwa kiberiti mbele ya malaika watakatifu na Mwanakondoo. Na moshi kutokana na kuungua kwao utasimama milele na milele. Hakutakuwa mapumziko, usiku na mchana kwa wale wamwabuduo mnyama au sanamu yake au wale wavaao alama ya jina lake.” Hii inamaanisha kuwa ni lazima watakatifu wa Mungu wawe na subira. Ni lazima wazitii amri za Mungu nakuendelea kumwamini Yesu. Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Liandike hili: Kuanzia sasa heri wale wanaokufa wakiwa wa Bwana.” Roho Mtakatifu anasema, “Ndiyo, hilo ni kweli. Watapumzika kutokana na kazi yao ngumu. Yale waliyotenda yatakaa pamoja nao.” Nikatazama, na mbele yangu, katika wingu jeupe, alikuwepo mmoja aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa na taji ya dhahabu kwenye kichwa chake na mundu mkali mkononi mwake. Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, akamwambia aliyekaa kwenye wingu, “Chukua mundu wako na ukusanye kutoka duniani. Wakati wa kuvuna umefika, na tunda limeiva duniani.” Hivyo aliyekaa kwenye wingu akaupitisha mundu wake juu ya dunia. Na dunia ikavunwa. Ndipo malaika mwingine akatoka hekaluni mbinguni. Malaika huyu naye alikuwa na mundu mkali. Na malaika mwingine, aliyekuwa msimamizi wa moto wa madhabahu akatoka madhabahuni. Akamwita malaika mwenye mundu mkali na kusema, “Chukua mundu wako wenye makali na ukusanye mafungu ya zabibu kutoka shamba la mizabibu duniani. Zabibu zimeiva duniani.” Malaika akaupitisha mundu juu ya dunia. Akakusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. Zabibu zikaminywa kwenye shinikizo nje ya mji. Damu ikatiririka kutoka kwenye shinikizo, ikanyanyuka juu kama vichwa vya farasi kwa urefu wa kilomita mia tatu. Ndipo nikaona ajabu nyingine mbinguni, ilikuwa kubwa na ya kushangaza. Walikuwepo malaika saba wenye mapigo saba. Haya ni mapigo ya mwisho kwa sababu baada ya haya, ghadhabu ya Mungu itakuwa imekwisha. Niliona kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Wale wote waliomshinda mnyama na sanamu yake na namba ya jina lake walikuwa wamesimama kando ya bahari. Watu hawa walikuwa na vinubi walivyopewa na Mungu. Waliuimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu na wimbo wa Mwanakondoo: “Mambo unayotenda ni makuu na ya kushangaza, Bwana Mungu Mwenye Nguvu. Njia zako ni sahihi na za kweli, mtawala wa mataifa. Watu wote watakucha wewe, Ee Bwana. Watu wote watalisifu jina lako. Mtakatifu ni wewe peke yako. Watu wote watakuja na kusujudu mbele yako, kwa sababu ni dhahiri kuwa wewe hutenda yaliyo haki.” Baada ya hili nikaona hekalu, mahali patakatifu pa Mungu mbinguni. Likiwa wazi; kisha malaika saba wenye mapigo saba wakatoka nje ya hekalu. Walikuwa wamevaa kitani safi inayong'aa. Wamevaa mikanda mipana ya dhahabu vifuani mwao. Kisha mmoja wa viumbe wenye uhai wanne akawapa malaika bakuli saba za dhahabu. Bakuli zilikuwa zimejaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. Hekalu lilikuwa limejaa moshi uliotoka katika utukufu na nguvu ya Mungu. Hakuna ambaye angeweza kuingia hekaluni mpaka mapigo saba ya malaika saba yamemalizika. Kisha nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni. Ikiwaambia malaika saba, “Nendeni mkazimimine bakuli saba zenye ghadhabu ya Mungu juu ya dunia.” Malaika wa kwanza akaondoka. Akaimimina bakuli yake duniani. Ndipo wale wote waliokuwa na alama ya mnyama na walioiabudu sanamu yake wakapata majipu mabaya yenye maumivu makali. Malaika wa pili akaimimina bakuli yake baharini. Bahari ikawa kama damu ya mtu aliyekufa. Kila kitu kinachoishi baharini kikafa. Malaika wa tatu akaimimina bakuli yake juu ya mito na chemichemi za maji. Mito na chemichemi za maji zikawa damu. Ndipo nikasikia malaika wa maji akimwambia Mungu: “Wewe ni yule uliyepo na uliyekuwepo daima. Wewe ni Mtakatifu. Uko sahihi kwa hukumu hizi ulizofanya. Watu walimwaga damu za watakatifu na manabii wako. Sasa umewapa watu hao damu ili wanywe. Hiki ndicho wanachostahili.” Pia nikasikia madhabahu ikisema: “Ndiyo, Bwana Mungu Mwenye Nguvu, hukumu zako ni za kweli na za haki.” Malaika wa nne akaimimina bakuli yake juu ya jua. Jua lilipewa nguvu kuwachoma watu kwa moto. Watu wakaungua kwa joto kali. Wakalilaani jina la Mungu, mwenye mamlaka juu ya mapigo haya. Lakini walikataa kubadili mioyo na maisha yao, na kumpa Mungu utukufu. Malaika wa tano akaimimina bakuli lake juu ya kiti cha enzi cha mnyama. Giza likaufunika ufalme wa mnyama. Watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu. Wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majipu waliyokuwa nayo. Lakini walikataa kubadili mioyo yao na kuyaacha maovu wanayotenda. Malaika wa sita akaimimina bakuli yake juu ya mto mkuu Frati. Maji yaliyokuwa mtoni yakakauka. Hili likaandaa njia kwa ajili ya watawala kutoka mashariki kuweza kupita. Kisha nikaona roho chafu tatu zilizoonekana kama vyura. Walitoka katika kinywa cha joka, kinywa cha mnyama, na kinywa cha nabii wa uongo. Roho hizi chafu ni roho za mapepo. Zina nguvu za kutenda miujiza. Nazo huenda kwa watawala wa ulimwengu wote na kuwakusanya kwa ajili ya mapigano siku ile Mungu Mkuu Mwenye Nguvu. “Sikilizeni! Nitakuja kama mwizi wakati msioutarajia. Heri watakaokuwa macho na waliovaa nguo zao. Hawatakwenda wakiwa uchi na kuona aibu watakapoonwa na watu.” Ndipo roho chafu zikawakusanya pamoja watawala pamoja mahali ambapo kwa Kiebrania panaitwa “Armagedoni”. Malaika wa saba akaimimina bakuli yake angani. Sauti kuu ikatoka hekaluni katika kiti cha enzi. Ikasema, “Imekwisha!” Kisha kukawa na mwako wa radi, kelele, ngurumo za radi na tetemeko kuu la nchi. Hili lilikuwa tetemeko kuu kuwahi kutokea tangu watu walipokuwepo duniani. Mji mkuu ukagawanyika vipande vitatu. Miji ya mataifa ikaharibiwa. Na Mungu hakusahau kuuadhibu Babeli Mkuu. Aliupa mji ule kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu yake kuu. Kila kisiwa kikatoweka na milima ikasawazika, hakukuwa milima yoyote tena. Mvua yenye mawe makubwa kutoka mbinguni ikawanyeshea watu. Mawe haya yalikuwa na uzito wa kilo 40 kila jiwe. Watu wakamlaani Mungu kwa sababu ya mvua hii ya mawe. Hali hiyo Ilitisha sana. Mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli sa akaja kuzungumza nami. Akasema, “Njoo, nami nitakuonesha adhabu itakayotolewa kwa kahaba maarufu. Ndiye yule aketiye juu ya maji mengi. Watawala wa dunia walizini pamoja naye. Watu wa dunia walilewa kutokana na mvinyo wa dhambi yake ya uzinzi.” Kisha malaika akanichukua mbali kwa Roho Mtakatifu mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke amekaa juu ya mnyama mwekundu. Mnyama alikuwa ameandikwa majina ya kumkufuru Mungu katika mwili wake wote. Alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. Mwanamke aliyekuwa juu yake alikuwa amevaa nguo za zambarau na nyekundu. Alikuwa anang'aa kutokana na dhahabu, vito na lulu alizokuwa amevaa. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu. Kikombe hiki kilijaa maovu na machukizo ya dhambi yake ya uzinzi. Alikuwa na jina kwenye kipaji cha uso wake. Jina hili lina maana iliyofichwa. Hiki ndicho kilichoandikwa: BABELI MKUU MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA DUNIA. Nikatambua kuwa mwanamke alikuwa amelewa. Alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu wa Mungu. Alikuwa amelewa kwa damu ya wale walioshuhudia imani yao katika Yesu Kristo. Nilipomwona mwanamke, nilishangaa sana. Kisha malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Nitakuambia maana iliyofichwa kuhusu mwanamke huyu na mnyama mwenye vichwa saba na pembe kumi anayeendeshwa na mwanamke huyu. Mnyama unayemwona alikuwa hai kwanza, lakini sasa si hai. Hata hivyo, atapanda kutoka kuzimu na kwenda kuangamizwa. Watu wanaoishi duniani watashangaa watakapomwona mnyama, kwa sababu aliwahi kuwa hai, hayuko hai, lakini atakuwa hai tena. Hawa ni watu ambao majina yao hayajawahi kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu. Unahitaji hekima kulielewa hili. Vichwa saba juu ya mnyama ni milima saba ambako mwanamke amekaa. Pia ni watawala saba. Watawala watano wamekwisha kufa tayari. Mmoja wa watawala anaishi sasa, na mtawala wa mwisho anakuja. Atakapokuja, atakaa kwa muda mfupi tu. Mnyama ambaye hapo kwanza alikuwa hai, lakini haishi tena ni mtawala wa nane. Naye ni mmoja wa watawala saba wa kwanza. Naye ataangamizwa. Pembe kumi ulizoziona ni watawala kumi. Watawala hawa kumi hawajapata falme zao, lakini watapata nguvu ya kutawala pamoja na mnyama kwa saa moja. Lengo la watawala hawa wote kumi linafanana. Nao watampa mnyama nguvu na mamlaka yao. Watafanya vita kinyume na Mwanakondoo. Lakini Mwanakondoo atawashinda, kwa sababu ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Pamoja naye watakuwepo wateule wake na wafuasi waaminifu, watu aliowaita kuwa wake.” Kisha malaika akaniambia, “Uliyaona maji ambako kahaba amekaa. Maji haya ni watu wengi, wa asili, mataifa, na lugha tofauti ulimwenguni. Mnyama na pembe kumi ulizoziona watamchukia kahaba. Watachukua kila kitu alichonacho na kumwacha akiwa uchi. Watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto. Mungu aliweka wazo katika akili zao kutenda yale yatakayotimiza kusudi lake. Walikubaliana kumpa mnyama nguvu zao kutawala mpaka yale aliyosema Mungu yamekamilika. Mwanamke uliyemwona ni mji mkuu ambao unatawala juu ya wafalme wa dunia.” Kisha nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Malaika huyu alikuwa na nguvu kuu. Utukufu wa malaika ukaing'arisha dunia. Malaika akapaza sauti akasema: “Ameteketezwa! Mji mkuu Babeli umeteketezwa! Umekuwa nyumba ya mapepo. Mji ule umekuwa najisi. Mji uliojaa kila aina ya ndege najisi. Ni mahali ambapo kila mnyama najisi na anayechukiwa anaishi. Watu wote wa dunia wamekunywa mvinyo wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu. Watawala wa dunia walizini pamoja naye, na wafanya biashara wa ulimwengu walitajirika kutokana na utajiri wa anasa zake.” Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema: “Enyi watu wangu, tokeni katika mji huo, ili msishiriki katika dhambi zake. Ili msiteseke kwa adhabu yoyote kuu atakayoipata. Dhambi za mji huo zimerundikana na kufika mbinguni. Mungu hajasahau makosa aliyotenda. Upeni mji huo sawasawa na ulivyowapa wengine. Mlipeni mara mbili kadiri ya alivyotenda. Mwandalieni mvinyo ulio na nguvu mara mbili ya mvinyo aliowaandalia wengine. Alijipa utukufu mwingi na kuishi kitajiri. Mpeni mateso mengi na huzuni nyingi. Kama vile utukufu na starehe aliyoifurahia. Hujisemea mwenyewe, ‘Mimi ni malkia nikaaye kwenye kiti changu cha enzi. Mimi si mjane; Sitakuwa na huzuni.’ Hivyo katika siku moja atateseka kwa njaa kuu, maombolezo na kifo. Atateketezwa kwa moto, kwa sababu Bwana Mungu anayemhukumu ni mwenye nguvu.” Watawala wa dunia waliozini pamoja naye na kushiriki utajiri wake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watalia na kuhuzunika kwa sababu ya kifo chake. Wataogopa mateso yake na kukaa mbali sana. Watasema: “Inatisha! Inatisha sana, Ee mji mkuu, ee Babeli, mji wenye nguvu! Adhabu yako imekuja katika saa moja!” Na wafanya biashara wa dunia watalia na kuhuzunika kwa ajili yake. Watahuzunika kwa sababu hakutakuwa hata mmoja wa kununua vitu wanavyouza; dhahabu, fedha, vito, lulu, nguo za kitani safi, nguo za zambarau, hariri na nguo nyekundu, aina zote za mti wa udi, na aina zote za vitu vilivyotengenezwa kutokana na pembe za wanyama, miti ya thamani, shaba, chuma, na marimari. Na mdalasini, viungo, uvumba, marhamu, ubani, mvinyo, mafuta ya mzeituni, unga safi, ngano, ng'ombe, kondoo, farasi, magari na watumwa, ndiyo hata maisha ya watu. Wafanya biashara watalia na kusema: “Ee Babeli, mambo mazuri uliyoyataka yamekuacha. Utajiri wako wote na vitu vya fahari vimetoweka. Hautakuwa navyo tena.” Wafanya biashara wataogopa mateso yake na watakaa mbali naye. Hawa ni wale waliotajirika kwa kumwuzia vitu hivyo. Watalia na kuhuzunika. Watasema: “Inatisha! Inatisha kwa mji mkuu! Alivalishwa kitani safi; alivaa zambarau na nguo nyekundu. Alikuwa anang'aa kwa sababu ya dhahabu, vito na lulu! Utajiri wote huu umeteketezwa kwa saa moja!” Kila nahodha, wote ambao husafiri katika meli, mabaharia na wote ambao hupata pesa kutokana na bahari walisimama mbali na Babeli. Waliuona moshi wa kuungua kwake. Walilia kwa sauti, “Hakukuwa na mji kama mji huu mkuu!” Walirusha mavumbi juu ya vichwa vyao na kulia kwa sauti kuu kuonesha huzuni kuu waliyokuwa nayo. Walisema: “Inatisha! Inatisha sana kwa mji mkuu! Wote waliokuwa na meli baharini walitajirika kwa sababu ya utajiri wake! Lakini umeteketezwa katika saa moja! Ufurahi kwa sababu ya hili, Ee mbingu! Furahini, watakatifu wa Mungu, mitume na manabii! Mungu amemhukumu kwa sababu ya kile alichowatendea ninyi.” Kisha malaika mwenye nguvu akainua jiwe kubwa. Jiwe hili lilikuwa kubwa kama jiwe kubwa la kusagia. Malaika akalitupia jiwe baharini na kusema: “Hivyo ndivyo mji mkuu Babeli utakavyotupwa chini. Hautaonekana tena. Ee Babeli, muziki wa wapigao vinanda na ala zingine waimbaji na tarumbeta, hautasikika tena ndani yako. Hakuna mfanyakazi afanyaye kazi atakayeonekana ndani yako tena. Sauti ya jiwe la kusagia haitasikika ndani yako tena. Mwanga wa taa hautang'aa ndani yako tena. Sauti za maarusi hazitasikika ndani yako tena. Wafanyabiashara wako walikuwa watu wakuu wa ulimwengu. Mataifa yote yalidanganyika kwa uchawi wako. Una hatia ya vifo vya manabii, na watakatifu wa Mungu, na vya wote waliouawa duniani.” Baada ya hili nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu mbinguni. Walikuwa wakisema: “Haleluya! Ushindi, utukufu na nguvu ni vyake Mungu wetu. Hukumu zake ni za kweli na za haki. Mungu wetu amemwadhibu kahaba. Ndiye aliyeiharibu dunia kwa uzinzi wake. Mungu amemwadhibu kahaba kulipa kisasi cha vifo vya watumishi wake.” Pia, watu hawa walisema: “Haleluya! Anaungua na moshi wake utasimama milele na milele.” Ndipo wazee ishirini na nne na viumbe wenye uhai wanne wakaanguka chini kusujudu wakamwabudu Mungu, akaaye kwenye kiti cha enzi. Wakasema: “Amina! Haleluya!” Sauti ikatoka kwenye kiti cha enzi na kusema: “Msifuni Mungu wetu, ninyi nyote mnaomtumikia! Msifuni Mungu wetu, ninyi nyote mlio wadogo na wakubwa mnaomheshimu!” Kisha nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu. Kilikuwa na kelele kama mawimbi ya bahari au radi. Watu walikuwa wakisema: “Haleluya! Bwana Mungu wetu anatawala. Ndiye Mwenye Nguvu, Mungu Mwenyezi. Tushangilie na kufurahi na kumpa Mungu utukufu! Mpeni Mungu utukufu, kwa sababu arusi ya Mwanakondoo imewadia. Na bibi arusi wa Mwanakondoo amekwisha jiandaa. Nguo ya kitani safi ilitolewa kwa bibi arusi ili avae. Kitani ilikuwa safi na angavu.” (Kitani safi inamaanisha mambo mazuri ambayo watakatifu wa Mungu waliyatenda.) Kisha malaika akaniambia, “Andika hili: Heri ni kwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo!” Kisha malaika akasema, “Haya ni maneno ya Mungu mwenyewe.” Kisha nikaanguka chini mbele miguuni pa malaika ili nimwabudu. Lakini malaika akaniambia, “Usiniabudu! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako na dada zako walio na ushuhuda kuhusu Yesu Kristo. Hivyo mwabudu Mungu! Kwa sababu ushuhuda kuhusu Yesu ndiyo roho ya unabii.” Kisha nikaona mbingu zimefunguka, na nikamwona farasi mweupe. Mpanda farasi aliitwa Mwaminifu na Kweli, kwa sababu ni wa haki katika maamuzi yake na kufanya vita. Macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. Alikuwa na taji nyingi kichwani mwake. Jina lilikuwa limeandikwa juu yake, lakini yeye peke yake ndiye aliyejua maana ya jina hilo. Alivaa vazi lililochovywa katika damu, na aliitwa Neno la Mungu. Majeshi ya mbinguni yalikuwa yanamfuata mpanda farasi mweupe. Walikuwa wanaendesha farasi weupe pia. Walikuwa wamevaa kitani nzuri, nyeupe na safi. Upanga mkali ulikuwa unatoka kwenye kinywa chake, upanga ambao angeutumia kuyashinda mataifa. Na atayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Atazikanyaga zabibu katika shinikizo la ghadhabu ya Mungu Mwenye Nguvu. Kwenye vazi lake na kwenye mguu wake alikuwa ameandikwa jina lake: MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA. Kisha nikaona malaika amesimama katika jua. Kwa sauti kuu malaika akawaambia ndege wote wanaoruka angani, “Kusanyikeni kwa ajili ya karamu kuu ya Mungu. Kusanyikeni mle miili ya watawala, majemadari na watu maarufu. Njooni mle miili ya farasi na wanaowapanda na miili ya watu wote, walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.” Kisha nikamwona mnyama na watawala wa dunia. Majeshi yao yalikusanyika pamoja ili kufanya vita kupigana na mpanda farasi mweupe na jeshi lake. Lakini mnyama na nabii wa uongo walikamatwa. Nabii wa uongo ndiye aliyefanya miujiza kwa ajili ya mnyama. Alitumia miujiza hii kuwahadaa wale waliokuwa na alama ya mnyama na walioabudu sanamu yake. Nabii wa uongo na mnyama walitupwa kwenye ziwa la moto linalowaka kwa baruti. Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kwenye kinywa cha mpanda farasi. Ndege wote walikula miili hii mpaka wakashiba. Nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni. Malaika alikuwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Malaika alimkamata joka, nyoka wa zamani ambaye pia anajulikana kama Ibilisi au Shetani. Malaika akamfunga joka kwa minyororo kwa muda wa miaka elfu moja. Kisha akamtupia kuzimu na akaifunga. Malaika akamfungia joka kuzimu ili asiweze kuwadanganya watu wa dunia mpaka miaka elfu moja iishe. Baada ya miaka elfu moja joka lazima aachiwe huru kwa muda mfupi. Kisha nikaona viti vya enzi na watu wamevikalia. Hawa ni wale waliopewa mamlaka ya kuhukumu. Na nikaona roho za wale waliouawa kwa sababu walikuwa waaminifu kwa kweli ya Yesu na ujumbe kutoka kwa Mungu. Hawakumwabudu mnyama wala sanamu yake. Hawakuipokea alama ya mnyama kwenye vipaji vya nyuso zao au mkononi mwao. Walifufuka na kutawala na Kristo kwa miaka elfu moja. (Wengine waliokufa hawakufufuka mpaka miaka elfu moja ilipokwisha.) Huu ni ufufuo wa kwanza. Heri walifufuliwa mara ya kwanza. Ni watakatifu wa Mungu. Mauti ya pili haina nguvu juu yao. Watakuwa makuhani wa Mungu na Kristo. Watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moja. Miaka elfu moja itakapokwisha, Shetani ataachiwa huru kutoka kwenye gereza lake. Atatoka na kwenda kuwadanganya mataifa katika dunia yote, mataifa yajulikanayo kama Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya watu kwa ajili ya vita. Kutakuwa watu wengi wasiohesabika kama mchanga katika ufukwe wa bahari. Nililiona jeshi la Shetani likitembea na kujikusanya ili kuizingira kambi ya watu wa Mungu na mji anaoupenda Mungu. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuliteketeza jeshi la Shetani. Na Shetani, yule aliyewadanganya watu hawa, alitupwa kwenye ziwa la moto pamoja na mnyama na nabii wa uongo. Watateseka kwa maumivu usiku na mchana milele na milele. Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe. Nikamwona aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha enzi. Dunia na anga vikamkimbia na kutoweka. Na nikaona wale waliokufa, wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi na vitabu vilifunguliwa. Na kitabu cha uzima kilifunguliwa pia. Watu walihukumiwa kwa yale waliyotenda, kama yalivyoandikwa katika vitabu. Bahari ikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Mauti na kuzimu zikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Watu wote hawa walihukumiwa kutokana na matendo yao. Mauti na kuzimu vilitupwa kwenye ziwa la moto. Ziwa hili la moto ni mauti ya pili. Na yeyote ambaye jina lake halikuonekana limeandikwa kwenye kitabu cha uzima alitupwa kwenye ziwa la moto. Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu na dunia ya kwanza vilikwisha kutoweka. Na sasa bahari haikuwepo. Nikauona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu. Ulikuwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyevalishwa kwa ajili ya mumewe. Nikasikia sauti kuu kutoka kwenye kiti cha enzi. Ikisema, “Makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu. Yeye ataishi pamoja nao. Na wao watakuwa watu wake. Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao naye atakuwa Mungu wao. Atafuta kila chozi kutoka machoni mwaona. Hakutakuwa na kifo tena, huzuni, kilio wala maumivu. Namna zote za zamani zimepita.” Aliyekaa kwenye kiti cha enzi akasema, “Tazama, sasa ninakiumba kila kitu upya!” Kisha akasema, “Andika hili, kwa sababu maneno haya ni kweli na ya kuaminiwa.” Akaniambia, “Imekwisha! Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Kila mwenye kiu nitampa bure maji kutoka kwenye chemichemi ya maji ya uzima. Wale wote watakaoshinda watapokea yote haya. Na nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watoto wangu. Lakini waoga, wanaokataa kuniamini, wafanyao mambo ya kuchukiza, wauaji, wazinzi, wachawi, waabuduo sanamu na waongo, nitawatupa katika ziwa linalowaka moto. Hii ni mauti ya pili.” Mmoja wa malaika saba akaja kwangu. Huyu alikuwa mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli saba zilizojaa mapigo saba ya mwisho. Malaika akasema, “Njoo huku. Nitakuonesha bibi arusi, mke wa Mwanakondoo.” Malaika akanichukua kwa Roho Mtakatifu mpaka kwenye mlima mkubwa na mrefu. Akanionyesha mji mtakatifu wa Yerusalemu. Mji ulikuwa ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu. Mji ulikuwa unang'aa kwa utukufu wa Mungu. Ulikuwa unang'aa kwa uangavu kama yaspi, kito cha thamani sana. Ulionekana kwa uwazi kama kioo. Mji ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mbili. Kulikuwa malaika kumi na mbili kwenye milango. Kwenye kila mlango kuliandikwa jina la kabila moja la Israeli. Yalikuwepo malango matatu upande wa mashariki, malango matatu kaskazini, malango matatu kusini, na malango matatu magharibi. Kuta za mji zilijengwa kwenye mawe kumi na mbili ya msingi. Kwenye mawe kulikuwa kumeandikwa majina ya mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo. Malaika aliyezungumza na mimi alikuwa na fimbo ya kupimia iliyotengenezwa kwa dhahabu. Alikuwa na fimbo hii ili kuupima mji, malango na ukuta wake. Mji ulijengwa kimraba. Urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Malaika aliupima mji kwa fimbo. Mji ulikuwa na urefu wa kilomita 2,400, upana wake ulikuwa kilomita 2,400, na kimo chake kwenda juu kilikuwa kilomita 2,400. Malaika akaupima ukuta pia. Kimo cha ukuta kilikuwa ni mita 60 kwenda juu. (Malaika alikuwa anatumia vipimo ambavyo watu hutumia.) Ukuta ulijengwa kwa yaspi. Mji ulijengwa kwa dhahabu safi, iliyo safi kama kioo. Mawe ya msingi wa ukuta wa mji yalikuwa na kila aina ya vito vya thamani ndani yake. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa yaspi, la pili lilikuwa yakuti samawi, la tatu lilikuwa kalkedoni, la nne lilikuwa zumaridi, la tano lilikuwa sardoniki, la sita lilikuwa akiki, la saba lilikuwa krisolitho, la nane lilikuwa zabarajadi, la tisa lilikuwa yakuti ya manjano, la kumi lilikuwa krisopraso, la kumi na moja lilikuwa hiakintho na la kumi na mbili lilikuwa amethisto. Malango kumi na mbili yalikuwa lulu kumi na mbili. Kila lango lilitengenezwa kwa lulu moja. Mitaa ya mji ilitengenezwa kwa dhahabu safi, inayong'aa kama kioo. Sikuona hekalu ndani ya mji. Bwana Mungu Mwenye Nguvu na Mwanakondoo ndiyo waliokuwa hekalu la mji. Mji haukuhitaji jua wala mwezi kuung'arizia. Utukufu wa Mungu uliupa mji mwanga. Mwanakondoo ndiye alikuwa taa ya mji. Mataifa watatembea katika mwanga unaotoka katika mji ule. Watawala wa dunia wataleta utukufu wao katika mji. Milango ya mji haitafungwa hata siku moja, kwa sababu hakutakuwa usiku huko. Ukuu na heshima ya mataifa vitaletwa katika mji. Kilicho najisi hakitaingia katika mji. Atendaye mambo ya kuchukiza na mwongo hawataingia katika mji huo. Walioandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwanakondoo tu, ndiyo watakaoingia katika mji huo. Malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, ulikuwa anga'avu kama kioo. Mto hutiririka kutoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. Hutiririka kupitia katika mtaa mkuu wa mji. Mti wa uzima uko kila upande wa mto, na huzaa tunda kila mwezi, mara kumi na mbili kwa mwaka. Majani ya mti ni kwa ajili ya kutibu mataifa. Katika mji ule hakuna mtu au kitu kitakachokuwa chini ya laana ya Mungu tena. Kiti cha ufalme cha Mungu na Mwanakondoo vitakuwa ndani ya mji. Watumishi wa Mungu watamwabudu yeye. Watauona uso wake. Jina la Mungu litaandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao. Hakutakuwa usiku tena. Watu hawatahitaji mwanga wa taa au mwanga wa jua. Bwana Mungu atawapa mwanga. Watatawala kama wafalme milele na milele. Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminiwa. Bwana, Mungu awavuviaye manabii, amemtuma malaika wake kuwaonesha watumishi wake mambo ambayo lazima yatokee hivi karibuni: ‘Sikiliza, Naja upesi! Heri anayetii maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.’” Mimi ni Yohana. Mimi ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Baada ya kuyasikia na kuyaona, niliinama chini kusujudu miguuni pa malaika aliyeyaonesha kwangu. Lakini malaika aliniambia, “Usinisujudie mimi! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako manabii, ni mtumishi kama wale wote wanaoyatii maneno yaliyo katika kitabu hiki. Msujudie Mungu!” Kisha malaika akaniambia, “Usiyafanye siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, wakati umekaribia kwa mambo haya kutokea. Kila atendaye mabaya aendelee kutenda mabaya. Yeyote aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Atendaye mema aendelee kutenda mema. Aliye mtakatifu aendelee kuwa mtakatifu.” “Sikiliza, nakuja upesi! Nakuja na ujira ili kumlipa kila mtu sawa sawa na matendo yake. Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho. Heri walioosha kanzu zao. Watakuwa na haki ya kula chakula kutoka kwenye mti wa uzima. Wanaweza kuingia katika mji kwa kupitia katika malango yake. Nje ya mji ni kwa ajili wale waishio kama mbwa; wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wapendao kudanganya na kujifanya wema. Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kukuambia mambo hayo kwa ajili ya makanisa. Mimi ni mzao wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi.” Roho Mtakatifu na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Kila asikiaye hili aseme pia, “Njoo!” Wote wenye kiu waje wanywe maji ya uzima bure ikiwa wanataka. Ninamwonya kila mtu anayesikia maneno ya unabii wa kitabu hiki: Ikiwa mtu yeyote ataongeza chochote kwa haya, Mungu atampa mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na ikiwa mtu yeyote akitoa sehemu yoyote ya maneno ya kitabu hiki cha unabii, Mungu ataondoa sehemu ya urithi wa mtu huyo katika mti wa uzima na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki. Yesu ndiye anayesema kwamba haya yote ni kweli. Sasa anasema, “Ndiyo, naja upesi.” Amina! Njoo, Bwana Yesu! Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja na watu wote.