Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa peke yake pasipo kitu, nalo giza lilivifunika vilindi, nayo Roho Ya Mungu ilikuwa imejitanda juu ya maji. Mungu akasema: Na uwe mwanga! Ndipo, mwanga ulipokuwa. Mungu akauona mwanga kuwa mwema, kisha Mungu akatenganisha mwanga na giza; mwanga Mungu akauita mchana, nalo giza akaliita usiku. Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya kwanza. Mungu akasema: Na uwe utando katikati ya maji, uyatenganishe maji na maji! Mungu akaufanya utando, akayatenga maji yaliyoko chini ya utando nayo maji yaliyoko juu ya utando; yakawa hivyo. Utando Mungu akauita mbingu. Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya pili. Mungu akasema: Maji yaliyoko chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, pakavu paonekane! Yakawa hivyo. Mungu akapaita pakavu nchi, nalo kusanyiko la maji akaliita bahari. Mungu akayaona kuwa mema. Kisha Mungu akasema: Nchi na ichipuze machipuko: mboga ziletazo mbegu na miti ya matunda iletayo matunda, kila mmmoja kwa namna yake, nayo yawe yenye mbegu zao ndani yao za kupandwa katika nchi. Yakawa hivyo. Ndipo, nchi ilipotoa machipuko: mboga ziletazo mbegu kwa namna zao na miti iletayo matunda, kila mmoja kwa namna yake, nayo yalikuwa yenye mbegu zao ndani yao, Mungu akayaona kuwa mema. Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya tatu. Mungu akasema: Na iwe mianga penye utando wa mbingu ya kuutenga mchana na usiku, iwe vielekezo vya kujulisha sikukuu na siku nyingine na miaka; nayo iwe mianga utandoni kwa mbingu ya kuiangaza nchi! Yakawa hivyo. Mungu akaifanya mianga miwili iliyo mikubwa: mwanga mkubwa wa kuutawala mchana nao mwanga mdogo wa kuutawala usiku pamoja na nyota. Mungu akaiweka utandoni kwa mbingu, ipate kingaza nchi na kuutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akayaona kuwa mema. Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya nne. Mungu akasema: Maji na yajae viumbe vya kuwa humo vyenye uzima, hata ndege na waruke juu ya nchi chini ya utando wa mbingu! Mungu akawaumba nyangumi wakubwa na viumbe vyote wanaokaa majini na kutembea humo, kila mmoja kwa namna yake, nao ndege wote warukao kwa mabawa, kila mmoja kwa namna yake. Mungu akawabariki kwamba: Zaeni, mwe wengi, mjae majini baharini, nao ndege na mawe wengi katika nchi! Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya tano. Mungu akasema: Nchi na itoe viumbe vyenye uzima vya kila namna, nyama wa nyumbani na wadudu na nyama wa porini wa kila namna! Yakawa hivyo. Mungu akawafanya nyama wa porini kila mmoja kwa namna yake na wadudu wote wa nchi kila mmoja kwa namna yake. Mungu akayaona kuwa mema. Kisha Mungu akasema: na tufanye mtu kwa mfano wetu, afanane na sisi, awatawale samaki wa baharini na ndege wa angani na nyama na nchi yote nzima na wadudu wote watambaao katika nchi! Mungu akamwumba mtu kwa mfano wake, mfano wake Mungu ndio, aliomwumbia, akamwumba kuwa mume na mke. Mungu akawabariki, Mungu akawaambia: Zaeni wana, mwe wengi, mwijaze nchi, kisha mwitiishe! Watawaleni samaki wa baharini na ndege wa angani na nyama wote pia watambaao katika nchi! Kisha Mungu akasema: Tazameni, nimewapa ninyi mboga zote zenye mbegu zilizoota katika nchi na miti yote izaayo matunda yenye mbegu ndani yao kuwa chakula chenu ninyi! Nao nyama wote wa nchi na ndege wote wa angani nao wote watambaao katika nchi walio viumbe vyenye uzima, nao chakula chao ni majani yote yanayolika. Yakawa hivyo. Mungu alipoyatazama yote, aliyoyafanya, akayaona kuwa mema sana. Pakawa jioni, pakawa asubuhi, ndio siku ya sita. Ndivyo, zilivyomalizika kuumbwa mbingu na nchi na vikosi vyao vyote. Siku ya saba Mungu alipozimaliza kazi zake zote, alizozifanya, akazipumzikia siku ya saba hizo kazi zake zote, alizozifanya; kwa hiyo Mungu akaibariki siku ya saba na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alizipumzikia kazi zake zote, alizozifanya za kuumba. Hivyo ndivyo, mbingu na nchi zilivyopata kuwapo hapo, zilipoumbwa. Siku hizo, Bwana Mungu alipozifanya nchi na mbingu, miti yote ya mashambani ilikuwa haijawa bado, nazo mboga zote za mashambani zilikuwa hazijaota bado, kwa kuwa Bwana Mungu alikuwa hajanyesha bado mvua katika nchi, tena hakuwako mtu wa kulima shamba. Lakini kungugu lilipopanda toka nchini likanywesha upande wa nje wa nchi yote. Naye Bwana Mungu alipomwumba mtu alimtengeneza na kutumia mavumbi ya nchi, kisha akampulizia puani mwake pumzi ya uzima; ndipo, mtu alipopata kuwa mwenye roho ya uzima. Kisha Bwana Mungu akapanda shamba huko Edeni upande wa maawioni kwa jua; ndiko, alikomweka huyo mtu, aliyemwumba. Bwana Mungu akaichipuza nchi miti yote ipendezayo kwa kutazamwa nayo ifaayo kwa kuliwa, napo hapo katikati ya shamba mti wa uzima na mti wa kujulia mema na mabaya. Tena kule Edeni kulitoka jito la kulinywesha hilo shamba, likajigawanya papo hapo shambani kuwa makono manne. Jina lake mto wa kwanza ni Pisoni, uliizunguka nchi yote ya Hawila iliyokuwa na dhahabu. Nayo dhahabu ya nchi hii ilikuwa nzuri; tena kulikuwako magwede na vito vya oniki. Jina lake mto wa pili ni Gihoni, nao ndio ulioizunguka nchi yote ya Kusi. Jina lake mto wa tatu ni Hidekeli, nao ndio unaopita upande wa maawioni kwa jua wa nchi ya Asuri. Nao mto wa nne ndio Furati. Bwana Mungu akamchukua Adamu, akamkalisha katika shamba la Edeni, alilime na kuliangalia. Kisha Bwana Mungu akamwagiza Adamu kwamba: Miti yote iliyomo humu shambani utaila, lakini mti wa kujulia mema na mabaya usiule! Kwani siku, utakapoula, huna budi kufa. Bwana Mungu akasema: Hiafai, mtu akiwa peke yake, nitamfanyizia mwenziwe wa kusaidiana naye. Bwana Mungu alipokwisha kuwatokeza katika nchi nyama wote wa porini na ndege wote wa angani akawapeleka kwa Adamu, aone, atakavyowaita; jina lake kila nyama mwenye uzima liwe lilo hilo, Adamu atakalomwita. Adamu akampa kila nyama wa nyumbani na kila ndege wa angani na kila nyama wa porini jila lake, lakini yeye Adamu hakuona mtu mwenziwe wa kusaidiana naye. Ndipo, Bwana Mungu alipomtia Adamu usingizi mzito, akalala usingizi kabisa. Kisha akamtoa ubavu wake mmoja, napo mahali pake akapaziba na nyama. Huo ubavu, aliomtoa Adamu, Bwana Mungu akauumba kuwa mke, akampeleka kwake Adamu. Adamu akasema: Kweli huyu ni mfupa utokao katika mifupa yangu, ni mwenye mwili utokao mwilini mwangu; kwa hiyo ataitwa mwanamke, kwa kuwa ametolewa katika mwanamume. Kwa sababu hii mtu atamwacha baba yake na mama yake, agandamiane na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Nao wote wawili, Adamu na mkewe, walikuwa wenye uchi, lakini hawakuona soni. Nyoka alikuwa mjanja kuliko nyama wote wa porini, Bwana Mungu aliowafanya. Naye akamwambia mwanamke: Kumbe Mungu amewakataza kuila miti yote iliyomo humu shambani? Lakini mwanamke akamwambia nyoka: Tunayala matunda ya miti iliyomo humu shambani; lakini matunda ya mti huu katikati ya shamba Mungu ametuambia: Msiyale! Msiyaguse, msipate kufa! Ndipo, nyoka alipomwambia mwanamke: kufa hamtakufa kabisa. Kwani Mungu anajua, ya kuwa siku, mtakapoula, macho yenu yatafumbuliwa, mwe kama Mungu mkijua mema na mabaya. Mwanamke alipoutazama huo mti akauona kuwa mwema wa kula, hata wa kuyapendeza macho, tena akauona, ya kuwa unapasa kutamaniwa kwa kuerevusha; ndipo, alipochuma tunda mojamoja, akala, akampa hata mumewe, naye akala. Ndipo, macho yao wote wawili yalipofumbuliwa, wakatambua, ya kuwa wako uchi; kwa hiyo wakashona majani ya mkuyu, wakayatumia ya kujifunga viunoni. Jua lilipokuwa limeponga, wakakisikia kishindo cha Bwana Mungu, akitembea shambani; ndipo, Adamu na mkewe walipojificha kwenye miti ya shamba, Bwana Mungu asiwaone. Bwanaa Mungu akamwita Adamu akisema: Uko wapi? Akajibu: Nimekisikia kishindo chako shambani, nikaogopa, kwa kuwa mimi ni mwenye uchi, nikajificha. Akasema: Ni nani aliyekuambia, ya kuwa wewe u mwenye uchi? Hukuula ule mti, niliokukataza, usiule? Naye Adamu akasema: Huyu mwanamke, uliyonipa kuwa nami, yeye amenipa tunda la mti ule, nikalila. Bwana Mungu akamwuliza mwanamke; Mbona umeyafanya hayo? Mwanamke akamwambia: Nyoka amenidanganya, nikala. Ndipo, Bwana Mungu alipomwambia nyoka: Kwa kuwa umeyafanya hayo, utakuwa umeapizwa wewe kuliko nyama wote wa nyumbani na wa porini, utajiburura kwa tumbo lako, ule mavumbi siku zako zote za kuwapo. Na niwachochee, mchukizane, wewe na huyu mwanamke, uzao wako na uzao wake, huyo atakuponda kichwa, nawe utamwuma kisigino. Kisha akamwambia mwanamke: Nitakupatia maumivu mengi, utakapopata mimba, itakuwa kwa machngu mengi, ukizaa watoto; ijapo yawe hivyo, utamtamani mumeo, naye atakutawala. Adamu naye akamwambia: Kwa kuwa umeiitikia sauti ya mkeo, ukaula ule mti, niliokuagiza kwamba: Usiule! nchi imeapizwa kwa ajili yako, uile na kuona uchungu siku zako zote za kuwapo. Itakuoteshea miiba na mibigili, nawe utakula majani ya shambani. Kwa jasho la uso wako utakula chakula, mpaka utakaporudi mchangani, kwani ndimo, ulimochukuliwa, kwani ndiwe mavumbi wewe, nayo mavumbi ndiyo, utakayokuwa tena. Adamu akamwita mkewe jina lake Ewa, kwa kuwa ndiye mama yao wote walio hai. Bwana Mungu akamtengenezea Adamu na mkewe ngozi za kuvaa, akawavika. Kisha Bwana Mungu akasema: Ninamwona Adamu, ya kuwa amekwisha kuwa kama mwenzetu kwa kujua mema na mabaya; labda sasa ataupeleka mkono wake, achume nayo matunda ya mti wa uzima na kuyala, apate kuwapo kale na kale. Kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika hilo shamba la Edeni, ailime nchi, alimochukuliwa. Ndiyo sababu, aliyomfukuzia Adamu, nao upande wa maawioni kwa jua wa shamba la Edeni akaweka Makerubi wenye panga zimulikazo moto pande zote, wailinde njia iendayo kwenye mti wa uzima. Adamu akamtambua mkewe Ewa, akapata mimba; kisha akamzaa Kaini, akasema: Nimepata mwanamume kwa Bwana. Tena akamzaa ndugu yake Abeli; naye Abeli akawa mchunga kondoo, lakini Kaini akawa mlima shamba. Siku zilipopita, Kaini akampelekea Bwana mazao ya shamba kuwa kipaji cha tambiko. Abeli naye akapeleka malimbuko ya kundi lake yenye manono. Bwana akamtazama Abeli na kipaji chake kwa kupendezwa, lakini Kaini na kipaji chake hakumtazama. Ndipo, makali ya Kaini yalipowaka moto sana, haata uso wake ukakunjamana. Naye Bwana akamwuliza Kaini: Mbona makali yako yamewaka moto? Mbona uso wako umekunjamana? Tazama, sivyo hivyo? Ukifanya mema utanielekezea macho; lakini usipofanya mema, ukosaji hulala mlangoni na kukutamani, lakini wewe sharti uushinde! Kisha Kaini akaongea na nduguye Abeli; lakini walipofika shambani, ndipo, Kaini alipomwinukia nduguye Abeli, akamwua. Naye Bwana alipomwuliza Kaini: Ndugu yako Abeli yuko wapi? akajibu: Sijui; je? Mimi ni mlezi wa ndugu yangu? Akamwuliza tena; Umefanya nini? Sauti za damu ya ndugu yako zinanililia huko nchini! Sasa wewe umeapizwa katika nchi hii iliyoasama kuipokea damu ya ndugu yako mkononi mwako. Utakapolima shamba, halitakupa tena liyawezayo kuzaa, utakuwa ukikimbiakimbia na kutangatanga katika nchi. Ndipo, Kaini alipomwambia Bwana: Manza zangu ni kubwa, haziwezekani kuondolewa. Tazama, umenifukuza leo hivi katika nchi hii, nami nitajificha, nisiuone uso wako tena, niwe mwenye kukimbiakimbia na kutangatanga katika nchi hii, kisha atakayeniona ataniua. Lakini Bwana akamwambia: Atakayemwua Kaini atalipizwa mra saba. Kisha Bwana akamtia Kaini alama, kila atakayemwona asimwue. Kisha Kaini akatoka machoni pa Bwana, akaenda kukaa katika nchi ya Nodi iliyoko ng'ambo ya Edeni. Kaini akamtambua mkewe, akapata mimba, kisha akamzaa Henoki. Naye Kaini alipojenga mji akauita huo mji kwa jina la mwanawe Henoki. Nenoki akapata mwana, ndiye Iradi, naye Iradi akamzaa Mehuyaeli, naye Mehuyaeli akamzaa Metusaeli, naye Metusaeli akamzaa Lameki. Lameki akajichukulia wake wawili, jina lake wa kwanza ni Ada, jina lake wa pili ni Sila. Ada akamzaa Yabali; yeye ndiye baba yao wanaokaa mahemani na kufuga nyama. Nalo jina la nduguye ni Yubali, yeye ndiye baba yao wapiga mazeze na mazomari. Sila naye akamzaa Tubalkaini, naye alikuwa mhunzi aliyejua kufua vyombo vyote vya shaba na vya chuma; naye umbu lake Tubalkaini alikuwa Nama. Lameki akawaambia wakeze Ada na Sila: Isikieni sauti yangu, ninyi wakeze Lameki! Yategeni masikio yenu, myasikie maneno yangu! Nimeua mtu, kwani aliniumiza, naye ni kijana, lakini alinitia mavilio. Kaini akilipizwa kisasi mara saba, Lameki na alipizwe kisasi mara sabini na saba. Adamu alipomtambua mkewe tena, akazaa mwana wa kiume, akamwita jina lake Seti (Pato), kwani alisema: Mungu amenipatia mzao mwingine mahali pake Abeli, kwa kuwa kaini alimwua. Seti naye alipozaliwa mwana akamwita jina lake Enosi. Siku hizo ndipo, watu walipoanza kulitambikia Jina la Bwana. Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku hiyo Mungu alipomwumba mtu alimtengeneza kwa mfano wake Mungu; akamwumba kuwa mume na mke, akawabariki, akawaita jina lao Adamu (Mtu) siku hiyo, walipoumbwa. Adamu alikuwa mwenye miaka 130 alipozaa mwana aliyefanana naye kwa kuwa mfano wake, akamwita jina lake Seti. Alipokwisha kumzaa Seti, siku zake Adamu zikawa tena miaka 800, akazaa wana wa kiume na wa kike. Siku zake Adamu, alizokuwapo, zote zikawa miaka 930, kisha akafa. Seti alikuwa mwenye miaka 105 alipomzaa Enosi. Alipokwisha kumzaa Enosi Seti akawapo miaka 807, akazaa wana wa kiume na wa kike. Siku zake Seti zote zikawa miaka 912, kisha akafa. Enosi alikuwa mwenye miaka 90 alipomzaa Kenani. Alipokwisha kumzaa Kenani Enosi akawapo miaka 815, akazaa wana wa kiume na wa kike. Siku zake Enosi zote zikawa miaka 905, kisha akafa. Kenani alikuwa mwenye miaka 70 alimpomzaa Mahalaleli. Alipokwisha kwisha kumzaa Mahalaleli, Kenani akawapo miaka 840, akazaa wana wa kiume na wa kike. Siku zake Kenani zote zikawa miaka 910, kisha akafa. Mahalaleli alikuwa mwenye miaka 65 alipomzaa Yaredi. Alipokwisha kumzaa Yaredi Mahalaleli akawapo miaka 830, akazaa wana wa kiume na wa kike. Siku zake Mahalaleli zote zikawa miaka 895, kisha akafa. Yaredi alikuwa mwenye miaka 162 alipomzaa Henoki. Alipokwisha kumzaa Henoki Yaredi akawapo miaka 800, akazaa wana wa kiume na wa kike. Siku zake Yaredi zote zikawa miaka 962, kisha akafa. Henoki alikuwa mwenye miaka 65 alipomzaa Metusela. Naye Henoki alifanya mwenendo wa kushikana na Mungu alipokwisha kumzaa Metusela akawapo miaka 300, akazaa wana wa kiume na wa kike. Siku zake Henoki zote zikawa miaka 365. Kwa kuwa Henoki alifanya mwenendo wa kushikana na Mungu, mara akawa hayuko tena, kwani Mungu alimchukua. Metusela alikuwa mwenye miaka 187 alipomzaa lameki. Alipokwisha kumzaa Lameki akawapo miaka 782, akazaa wana wa kiume na wa kike. Siku zake Metusela zote zikawa miaka 969, kisha akafa. Lameki alikuwa mwenye miaka 182 alipozaa mwana. Akamwita jinala lake Noa (Tulia) kwa kwamba: Huyu ndiye atakayetutuliza mioyo kwa ajili ya kazi zetu, mikono yetu inazozifanya kwa uchungu katika nchi, aliyoiapiza Bwana. Alipokwisha kumzaa Noa Lameki akawapo miaka 595, akazaa wana wa kiume na wa kike. Siku zake Lameki zote zikawa miaka 777, kisha akafa. Noa alikuwa mwenye miaka 500 alipozaa wana; Semu, Hamu na Yafeti. Watu walipoanza kuwa wengi katika nchi, nao wna wa kike walipozaliwa kwao, nao wana wa Mungu walipowaona wana wa kike wa watu kuwa wazuri, wakajichukulia wake kwao wote, waliowachagua. Ndipo, Bwana aliposema: Roho yangu haiwezi kubishana na watu kale na kale, kwani kwa hivyo, walivyopotea, mioyo yao imegeuka kuwa nyama tupu. Basi, siku zao na ziwe bado miaka 120. Siku zile walikuwako katika nchi nao watu walio majitu; hata baadaye siku zote wana wa Mungu walipoingia kwao wana wa kike na watu, nao waliwazalia wana; hawa ndio wale wenye nguvu waliojipatia jina kuu tangu kale. Bwana alipoona, ya kuwa ubaya wa watu ni mwingi katika nchi, nayo yote, waliyoyalinganya na kuyawaza mioyoni mwao, ni mabaya tu siku zote, ndipo, Bwana alipojuta, akaumizwa sana moyoni mwake, ya kuwa aliwafanya watu wa kukaa katika nchi. Kwa hiyo Bwana akasema: Nitawafuta watu, niliowaumba, watoweke katika nchi, wao watu nao nyama na wadudu na ndege wa angani, kwani ninajuta, ya kuwa niliwafanya. Noa akapata upendeleo machoni pake Bwana. Hivi ndivyo vizazi vyake Noa: Noa alikuwa mtu mwongofu mwenye kumcha Mungu miongoni mwao, aliozaliwa nao, kwani Noa alifanya mwenendo wa kushikana na Mungu. Noa akazaa wana watatu: Semu, Hamu na Yafeti. Nayo nchi ilikuwa imegeuka kuwa mbaya machoni pake Mungu, hiyo nchi ikijaa ukorofi. Mungu alipoitazama nchi akaiona kuwa mbaya, kwani wote wenye miili walishika njia mbaya katika nchi. Ndipo, Mungu alipomwambia Noa: Mwisho wao wote wenye miili umefika machoni pangu, kwani wameijaza nchi makorofi yao, kwa hiyo wataniona, nikiwaangamiza pamoja na nchi. Jitengenezee chombo kikubwa sana cha miti ya mivinje! Humo chomboni ndani ukate vyumba! Kisha kipake lami upande wa ndani nao wa nje! Navyo ndivyo, utakavyokitengeneza: urefu wa hicho chombo uwe mikono 30, nao upana wake mikono 50, nao urefu wake wa kwenda juu mikono 300. Juu yake hicho chombo utengeneze mahali pa kuingizia mwanga, upana wake uwe mkono mmoja; napo upafanye, pazunguke huko juu, nao mlango wa chombo uweke mbavuni pake! Utengeneze nayo madari matatu, la chini, la kati, la juu! Kwani tazama: Mimi nitaleta mafuriko ya maji juu ya nchi, niwaangamize wote wenye miili walio na pumzi za uzima, walioko chini ya mbingu; wote pia wanaokaa katika nchi sharti wafe. Lakini wewe nitakuwekea agano: Utaingia mle chomboni, wewe na wanao na mkeo nao wake wa wanao pamoja na wewe. Tena miongoni mwao nyama wote wenye miili utaingiza mle chomboni wawili wawili, wa kiume na wa kike, niwaponye pamoja na wewe, nao ndege wa kila namna nao nyama wa nyumbani wa kila namna, nao wadudu wote wa nchi wa kila namna; wao wote na waingie kwako wawili wawili, niwaponye. Kisha wewe jichukulie vilaji vyote vinavyoliwa, uvikusanye kwako, viwe chakula chako wewe nacho chao. Nao akayafanya yote; kama Mungu alivyomwagiza, ndivyo, alivyoyafanya. Bwana akamwambia Noa: Ingia chomboni wewe na mlango wako wote! Kwani nimekuona kuwa mwongofu machoni pangu katika kizazi hiki. Namo miongoni mwao nyama wote wa nyumbani wanaotakata jichukulie saba saba, mume na mkewe, nao nyama wa nyumbani wasiotakata chukua wawili wawili tu, mume na mkewe! Nao ndege wa angani chukua saba saba wa kiume na wa kike, niwaponye wa kuzaa katika nchi yote nzima. Kwani ziko bado siku saba, ndipo, mimi nitakaponyesha mvua siku 40 mchana kutwa na usiku kucha, niwatoweshe katika nchi yote nzima wote pia wanaosimama bado, niliowaumba mimi. Noa akayafanya yote, kama Bwana alivyomwagiza. Naye Noa alikuwa mwenye miaka 600 hapo, mafuriko ya maji mengi yalipokuwa juu ya nchi. Noa akaingia chomboni pamoja na wanawe na mkewe na wake wa wanawe, mafuriko ya maji yalipokuw hayajawa bado. Nao nyama wanaotakata nao wasiotakata nao ndege nao wote wanaotambaa katika nchi, wakaingia wawili wawili chomboni mwake Noa, wa kiume na wa kike, kama Mungu alivyomwagiza Noa. Ikawa, zile siku saba zilipokwisha pita, mafuriko ya maji yakawa juu ya nchi. Katika mwaka wa 600 wa siku zake Noa katika mwezi wa pili siku ya kumi na saba ya mwezi siku hiyo ndipo, chemchemi zote za vilindi vikuu zilipobubujika, nayo madirisha ya mbinguni yakafunguliwa, mvua ikanyesha katika nchi siku 40 mchana kutwa na usiku kucha. Siku ileile Noa akaingia chomboni, na Semu na Hamu na Yafeti, wanawe Noa, na mkewe Noa, nao wake watatu wa wanawe pamoja nao. Tena pamoja nao nyama wote wa porini wa kila namna nao nyama wote wa nyumbani wa kila namna na wadudu wote wanaotambaa katika nchi wa kila namna na wote walioweza kuruka wa kila namna na ndege wote nao wote wenye mabawa; wakaingia chomboni kwake Noa wawili wawili miongoni mwao wote wenye miili walio na pumzi za uzima. Miongoni mwao hao wote wenye miili wakaja mume na mke, wakaingia kwake, kama Mungu alivyomwagiza. Kisha Bwana akamfungia. Basi, yakawako mafuriko ya maji siku 40 juu ya nchi; maji yalipokuwa mengi yakakieleza kile chombo, kikawa juu ya nchi. Hayo maji yakakaza kuwa yenye nguvu, yakawa mengi sana juu ya nchi, nacho kile chombo kikaelea juu ya maji. Hayo maji yalipokaza kuwa yenye nguvu yakapanda, yakapanda juu ya nchi, mpaka ikifunikizwa milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu; hayo maji yakaipita juu mikono 15; ndivyo, milima ilivyofunikizwa. Ndipo, walipokufa wote wenye miili wao waliotembea katika nchi: ndege na nyama wa nyumbani na nyama wa porini na wadudu wote waliotambaa katika nchi, nao watu wote. Wote pia waliovuta puani mwao pumzi za roho yenye uzima, miongoni mwao wote waliokaa pakavu wakafa. Ndivyo, alivyowatowesha wote waliosimama juu ya nchi kuanzia watu, tena nyama na wadudu nao ndege wa angani, walitoweshwa wote katika nchi, akasalia Noa peke yake pamoja nao waliokuwa naye mle chomboni. Nayo hayo maji yakakaza kuwa yenye nguvu zizo hizo juu ya nchi siku 150. Kisha Mungu akamkumbuka Noa na wale nyama wote nao nyama wa nyumbani waliokuwa naye chomboni; ndipo, Mungu alipovumisha upepo juu ya nchi; kwa hiyo maji yakaanza kupwa. Nazo chemchemi za vilindini zikazibwa, nayo madirisha ya mbinguni yakafungwa, nazo mvua zilizotoka mbinguni zikakomeshwa. Kwa hiyo maji yakaanza kutoka tena juu ya nchi, yakaenda vivyo hivyo na kurudi mahali pao, baada ya siku 150 yakawa yamepunguka. Kisha kile chombo kikaja kutua kileleni kwa milima ya Ararati katika mwezi wa saba siku ya kumi na saba ya mwezi. Nayo maji yakawa yakiendelea kupunguka mpaka mwezi wa kumi. Siku ya kwanza ya mwezi katika mwezi wa kumi ndipo, vichwa vya milima vilipotokea. Siku 40 zilipopita tena, Noa akafungua dirisha la chombo, alilolifanya, akatoa kunguru; huyu akaruka kwenda na kurudi kwenda na kurudi, mpaka maji yakikauka katika nchi. Kisha akatoa njiwa kwake, aone, kama maji yamekauka katika nchi. Huyo njiwa asipoona pa kutulia kwa nyayo za miguu yake akarudi kwake chomboni, kwani maji yalikuwa yangaliko juu ya nchi yote; naye akautoa mkono wake, akamchukua na kumwingiza kwake chomboni. Akangoja tena siku saba nyingine, kisha akatoa tena njiwa mle chomboni. Huyu njiwa aliporudi kwake saa za jioni, akaona mdomoni mwake jani la mchekele, alilolivunja. Ndipo, Noa alipotambua, ya kuwa maji yamepunguaka katika nchi. Akangoja tena siku saba nyingine, akatoa tena njiwa, naye hakurudi tena kwake. Ikawa katika mwaka wa 601 katika mwezi wa kwanza siku ya kwanza ya mwezi, ndipo, maji yalipokauka na kutoweka juu ya nchi. Naye Noa alipokiondoa kipaa cha chombo kutazama, akaona, ya kuwa nchi imekauka juu. Katika mwezi wa pili siku ya ishirini na saba ya mwezi nchi ilikuwa imekauka kabisa. Mungu akasema na Noa kwamba: Toka chomboni, wewe na mkeo na wanao na wake wa wanao walio pamoja na wewe! Nao nyama wote walioko kwako, wao wote wenye miili: ndege na nyama na wadudu wote waliotambaa katika nchi watoe pamoja na wewe, wajiendee po pote katika nchi, wapate kuzaa na kuwa wengi tena katika nchi! Ndipo, Noa alipotoka na wanawe na mkewe na wake wa wanawe waliokuwa naye; tena nyama wote na wadudu wote na ndege wote nao wote waliotambaa katika nchi wakatoka chomboni, walimokuwa, kabila kwa kabila. Kisha Noa akamjengea Bwana pa kumtambikia, akatoa wengine katika nyama wote wa nyumbani wanaotakata na katika ndege wote wanaotakata, akawatolea hapo pa kumtambikia Bwana kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima. Bwana aliposikia huo mnuko wa kumpendeza Bwana akasema moyoni mwake: Sitaiapiza nchi tena kwa ajili ya watu, kwani mawazo ya mioyo ya watu ni mabaya tangu utoto wao, wala sitawapiga tena wote walio hai, kama nilivyofanya. Siku zote, nchi itakazokuwapo, hakutakoma tena kupanda na kuvuna, baridi na jua kali, kipupwe na kiangazi, mchana na usiku. Mungu akambariki Noa na wanawe na kuwaambia: Zaeni wana, mwe wengi, mwijaze nchi! Nyama wote wa nchi nao ndege wote wa angani sharti wawaogope ninyi na kuwastuka, wote pia wanaotembea katika nchi nao samaki wote wa baharini wametiwa mikononi mwenu. Nyama wote wanaotembea wenye uzima ni chakula chenu; kama nilivyowapa maboga yenye majani, ninawapa sasa wao wote nao. Lakini nyama walio wazima bado, maana walio wenye damu zao msiwale! Nazo damu zenu na roho zenu nitazilipiza, kweli nitazilipiza kwa nyama wote nako kwa watu, roho ya mtu nitailipiza kwa mtu mwenziwe. Atakayemwaga damu ya mtu damu yake nayo sharti imwagwe na mtu, kwa kuwa Mungu alimfanya mtu kwa mfano wake. Nanyi zaeni wana, mwe wengi! Ijazeni nchi mkiwa wengi huku! Kisha Mungu akamwambia Noa na wanawe waliokuwa naye kwamba: Tazameni, mimi sasa ninawawekea agano langu ninyi nao wa uzao wenu wajao nyuma yenu nao nyama wote wenye uzima waliokuwa nanyi: ndege na nyama wa nyumbani na nyama wote wa porini waliokuwa nanyi, wao wote waliotoka mle chomboni, ndio nyama wote pia wa huku nchini. Nalo agano langu, ninalowawekea ninyi, ni hili: Wao wote wenye miili hawatatoweshwa tena na mafuriko ya maji, wala hayatakuwako tena mafuriko ya maji ya kuiangamiza nchi. Kisha Mungu akasema: Agano hili, mimi ninalolifanya nanyi nao nyama wote wenye uzima wanaokaa kwenu, litakuwa nalo lao vizazi vya kale na kale, nacho kielekezo chake ni hiki: nimeuweka upindi wangu mawinguni, nao utakuwa kielekezo cha agano, mimi nililoliagana na nchi. Itakapokuwa, nikitanda mawingu mengi juu ya nchi, huo upindi utaoneka mawinguni; ndipo, nitakapolikumbuka agano langu mimi, nililoliagana nanyi nao wote wenye roho za uzima, ndio wote wenye miili, ya kwamba: Hayatakuwako tena mafuriko ya maji ya kuwaangamiza wote wenye miili. Upindi huo utakapokuwa mawinguni, nitautazama, nilikumbuke agano la kale na kale, mimi Mungu nililoliagana nao wote wenye roho za uzima, ndio wenye miili wote wanaokaa huku nchini. Kisha Mungu akamwambia Noa: Hiki ndicho kielekezo chaagano, nililokuwekea wewe nao wenye miili wote wanaokaa huku nchini. Wana wa Noa waliotoka chomboni walikuwa Semu na Hamu na Yafeti, naye Hamu ndiye baba yao Wakanaani. Hawa watatu walikuwa wana wa Noa; toka kwao hawa watu wakaineza nchi yote. Noa alipoanza kulima shamba, akapanda shamba la mizabibu. Lakini alipokunywa mvinyo akalewa, akalala hemani pasipo kujifunika. Hamu, baba yao Wakanaani, alipouona uchi wa baba yake, akawasimulia ndugu zake wawili huko nje. Ndipo, Semu na Yafeti walipochukua nguo, wakaiweka mabegani kwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao, macho yao yakitazama mbele, wasiuone uchi wa baba yao. Noa alipolevuka katika ulevi wa mvinyo, naye alipoyatambua, mwanawe mdogo aliyomfanyizia, ndipo aliposema: Kanaani na awe ameapizwa! Sharti awe mtumwa wa watumwa kwa ndugu zake! Kisha akasema: na atukuzwe Bwana, Mungu wa Semu! Naye Kanaani sharti awe mtumwa wake! Mungu na ampanulie naye Yafeti, apate kukaa mahemani mwa Semu! Naye Kanaani sharti awe mtumwa wake! Baada ya mafuriko ya maji Noa akawapo miaka 350. Hivyo siku zote za kuwapo kwake Noa zikawa miaka 950, kisha akafa. Hivi ndivyo vizazi vya wana wa Noa: Semu, Hamu na Yafeti; nao walizaliwa wana baada ya mafuriko ya maji. Wana wa Yafeti ni Gomeri na Magogi na Madai na Yawani na Tubali na Meseki na Tirasi. Nao wana wa Gomeri ni Askenazi na Rifati na Togarma. Nao wana wa Yawani ni Elisa na Tarsisi na Wakiti na Wadodani. Kwao hao walijitenga wenyeji wa visiwa vya wamizimu, wakae katika nchi zao, kila kabila lenye msemo wake; hivyo ndivyo, koo zao zilivyopata kuwa mataifa. Nao wana wa Hamu ni Kusi (Nubi) na Misri na Puti na Kanaani. Nao wana wa Kusi ni Seba na Hawila na Sabuta na Rama na Sabuteka. Nao wana wa Rama ni Saba na Dedani. Kusi akamzaa Nimurodi; ndiye aliyeanza kuwa mwenye nguvu katika nchi. Alikuwa mwindaji mwenye nguvu mbele ya Bwana, kwa hiyo watu husema: Mwindaji mwenye nguvu mbele ya Bwana kama Nimurodi. Mwanzo wa ufalme wake ulikuwa huko Babeli na Ereki na Akadi na Kalne katika nchi ya Sinari. Akatoka katika nchi hii kwenda Asuri, akajenga huko Niniwe na Rehoboti, Iri na Kala, tena Reseni katikati ya Niniwe na Kala, nao ni mji mkubwa. Naye Misri akawazaa Waludi na Waanami na Walehabi na Wanafutuhi na Wapatirusi na Wakasiluhi, ambao Wafilisti walitoka kwao, na Wakafutori. Naye Kanaani akamzaa Sidoni, mwanawe wa kwanza, na Hiti; tna Myebusi na Mwamori na Mgirgasi na Mhiwi na Mwarki na Msini, na Mwarwadi na Msemari na Mhamati. Halafu koo zao Wakanaani zikasambaa. Mipaka yao Wakanaani ilianza Sidoni, ikafika Gerari na Gaza, ikaendelea kufika Sodomu na Gomora na Adima na Seboimu mpaka Lasa. Hawa ndio wana wa Hamu, walivyokuwa wenye koo zao na miseo yao, tena ndivyo, mataifa yao walivyokaa katika nchi zao. Naye Semu, baba yao wana wote wa Eberi, aliyekuwa kaka yake yafeti, akazaliwa wana. Wana wa Semu ni Elamu na Asuri na Arpakisadi na Ludi na Aramu. Nao wana wa Aramu ni Usi na Huli na Geteri na Masi. Naye Arpakisadi akamzaa Sela, naye Sela akamzaa Eberi. Naye Eberi akazaliwa wana wawili, jina lake wa kwanza ni Pelegi (Gawanyiko), kwa kuwa siku zake ndipo, nchi hii ilipogawanyika, nalo jina la nduguye ni Yokitani. Naye Yokitani akamzaa Almodadi na Selefu na Hasarmaweti na Yera, na Hadoramu na Uzali na Dikla, na Obali na Abimaeli na Saba, na Ofiri na Hawila na Yobabu. Hawa wote ndio wana wa Yokitani. Nayo makao yao yalianza Mesa, yakafika mpaka mlima wa Sefari ulioko upande wa maawioni kwa jua. Hawa ndio wana wa Semu, walivyokuwa wenye koo zao na misemo yao, tena ndivyo, mataifa yao yalivyokaa katika nchi zao. Hizi ndizo koo zao wana wa Noa, walivyofuatana kuzaliwa na kugawanyika kuwa mataifa. Kwa hiyo walijitenga kuwa mataifa yaliyokaa katika nchi baada ya mafuriko ya maji. Watu wa nchi yote nzima walikuwa wenye msemo mmoja, nayo maneno yalikuwa yaleyale mamoja. Ikawa, walipoondoka kwenda upande wa maawioni kwa jua, wakaona bonde pana katika nchi ya Sinari, wakakaa huko. Kisha wakasemezana wao kwa wao: Haya! Na tuumbe matofali, tuyachome moto! Haya matofali yakawa mawe yao ya kujenga, nao udongo ukawa chokaa yao. Wakasema: Haya! Na tujijengee mji wenye mnara, nayo ncha yake ifike mbinguni, tujipatie jina, tusije kusambazwa katika nchi zote za duniani! Ndipo, Bwana aliposhuka, autazame huo mji na mnara, wana wa Adamu walioujenga. Bwana akasema: Ninawaona watu hawa kuwa ukoo mmoja tu, nao msemo wao wote ni mmoja tu vilevile. Nao huu ndio mwanzo tu wa matendo yao; sasa yote, watakayoyawaza mioyoni kuyafanya, hakuna lo lote litakalowashinda. Haya! Na tushuke, tuuvuruge msemo wao huko, mtu asiusikie msemo wa mwenziwe! Hivyo ndivyo, Bwana alivyowatawanya na kuwatoa huko, wajiendee kukaa katika nchi zote. Ndipo, walipoacha kuujenga ule mji. Kwa sababu hiyo wakauita jina lake Babeli (Mvurugo), kwa kuwa huko ndiko, Bwana alikouvuruga msemo wa watu wote wa huku nchini, akawatawanya na kuwatoa huko, wajiendee kukaa katika nchi zote. Hivi ndivyo vizazi vya Semu: Semu alipokuwa mwenye miaka 100 akamzaa Arpakisadi katika mwaka wa pili baada ya mafuriko ya maji. Semu alipokwisha kumzaa Arpakisadi akawapo miaka 500, akazaa wana wa kiume na wa kike. Arpakisadi alipokuwa mwenye miaka 35 akamzaa Sela. Arpakisadi alipokwisha kumzaa Sela akawapo miaka 403, akazaa wana wa kiume na wa kike. Sela alipokuwa mwenye miaka 30 akamzaa Eberi. Sela alipokwisha kumzaa Eberi akawapo miaka 403, akazaa wana wa kiume na wa kike. Eberi alipokuwa mwenye miaka 34 akamzaa Pelegi. Eberi alipokwisha kumzaa Pelegi akawapo miaka 430, akazaa wana wa kiume na wa kike. Pelegi alipokuwa menye miaka 30 akamzaa Reu. Pelegi alipokwisha kumza Reu akawapo miaka 209, akazaa wana wa kiume na wa kike. Reu alipokuwa mwenye miaka 32 akamzaa Serugi. Reu alipokwisha kumzaa Serugi akawapo miaka 207, akazaa wana wa kiume na wa kike. Serugi alipokuwa mwenye miaka 30 akamzaa Nahori. Serugi alipokwisha kumzaa Nahori akawapo miaka 200, akazaa wana wa kiume na wa kike. Nahori alipokuwa mwenye miaka 29 akamzaa Tera. Nahori alipokwisha kumzaa Tera, akawapo miaka 119, akazaa wana wa kiume na wa kike. Tera alipokuwa mwenye miaka 70 akamzaa Aburamu na Nahori na Harani. Hivi ndivyo vizazi vya Tera: Tera akamzaa Aburamu na Nahori na Harani. Naye Harani akamzaa Loti. Harani akafa machoni pake baba yake Tera katika nchi alikozaliwa, ndiko Uri wa Wakasidi. Kisha Aburamu na Nahori wakajichukulia wanawake, mkewe Aburamu jina lake Sarai, naye mkewe Nahori jina lake Milka, binti Harani aliyekuwa baba yao Milka na Isika. Lakini Sarai alikuwa mgumba, asipate mtoto. Kisha Tera akamchukua mwanawe Aburamu na Loti, mwana wa mwanawe Harani, na mkwewe Sarai, mkewe mwanawe Aburamu, wakatoka naye mle Uri wa Wakasidi kwenda katika nchi ya Kanaani, nao walipofika Harani wakakaa huko. Nazo siku zake Tera zilikuwa miaka 205, naye akafa huko Harani. Bwana akamwambia Aburamu: Toka katika nchi yako kwenye ndugu zako namo nyumbani mwa baba yako, uende katika nchi, nitakayokuonyesha! Nitakufanya kuwa taifa kubwa, nitakubariki na kulikuza jina lako, uwe mbaraka. Nitawabariki watakaokubariki, naye atakayekuapiza nitamwapiza. Mwako ndimo, koo zote za nchini zitakamobarikiwa. Ndipo, Aburamu alipoondoka, kama Bwana alivyomwambia, naye Loti akaenda naye. Naye Aburamu alikuwa mwenye miaka 75 alipotoka Harani. Aburamu akamchukua mkewe Sarai na Loti, mwana wa nduguye, nayo mapato yao yote, waliyojipatia, nao watu wao wote, waliowapata huko Harani; ndivyo, walivyotoka kwenda katika nchi ya Kanaani. Walipofoka katika nchi ya Kanaani, Aburamu akaikata hiyo nchi, mpaka akifika mahali pa Sikemu penye mvule wa More; siku zile Wakanaani walikaa katika nchi hiyo. Huko Bwana akamtokea Aburamu, akamwambia: Nchi hii nitawapa wao wa uzao wako! Ndipo, alipomjengea Bwana pa kumtambikia, kwa kuwa alimtokea hapo. Kisha akaondoka huko kwenda kwenye mlima ulioko upande wa maawioni kwa jua kwa Beteli, akalipiga hema lake mahali, Beteli ulipokuwa upande wa baharini nao Ai upande wa maawioni kwa jua; huko akajenga pa kumtambikia Bwana, akalitambikia Jina la Bwana. Kisha Aburamu akaondoka huko, akaendelea kusafiri upande wa kusini. Njaa ilipoingia katika nchi ile, Aburamu akashuka kwenda Misri kukaa ugenini huko, kwani njaa ilikuwa kubwa. Walipofika karibu kuingia Misri akamwambia mkewe Sarai: Tazama, ninakujua kuwa mwanamke mwenye mwili mzuri. Itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema: Huyu ni mkewe. Basi, mimi wataniua, lakini wewe watakuacha, ukae. Kwa hiyo sema, ya kuwa u dada yangu, nipate mema kwa ajili yako! Hivyo ndivyo, roho yangu nayo itakavyopona kwa ajili yako. Ikawa, Aburamu alipoingia Misri, Wamisri wakamwona mke kuwa mzuri sana. Nao wakuu wa Farao walipomwona, wakamsifia Farao; ndipo, huyo mwanamke alipochukuliwa kukaa nyumbani mwa Farao. Naye akamfanyia Aburamu mema kwa ajili yake, akapata mbuzi na kondoo na ng'ombe na punda na watumwa wa kiume na wa kike na punda wa kike na ngamia. Lakini Bwana akampiga Farao mapigo makuu, nao mlango wake, kwa ajili ya Sarai, mkewe Aburamu. Ndipo, Farao alipomwita Aburamu, akamwambia: Kwa nini umenifanyizia hivyo usiponiambia, ya kuwa ni mkeo? Kwa nini umesema: Ni dada yangu, mimi nikamchukua kuwa mke wangu? Sasa mchukue huyu mkeo, uende zako! Kisha Farao akamwagizia watu, wampeleke yeye na mkewe na mali zake zote. Ndipo, Aburamu alipotoka Misri kwenda kwao upande wa kusini, yeye na mkewe nao wote, aliokuwa nao, hata Loti alikuwa naye. Naye Aburamu alikuwa mwenye mali nyingi sana za makundi na za fedha na za dhahabu. Akaendelea kusafiri hapohapo upande wa kusini mpaka kufika Beteli mahali pale, hema lake lilipokuwa kwanza katikati ya Beteli na Ai; ndipo hapo, Aburamu alipojenga pa kwanza pa kumtambikia Bwana na kulitambikia Jina lake. Lakini Loti naye aliyesafiri pamoja na Aburamu alikuwa mwenye mbuzi na kondoo na ng'ombe na mahema. Kwa hiyo haikuwezekana, wakae pamoja katika nchi ile, kwa kuwa mapato yao yalikuwa mengi, kweli hawakuweza kukaa pamoja. Kwa hiyo wachunga makundi ya Aburamu waligombana nao wachunga makundi ya Loti, kwani Wakanaani na Waperizi nao walikaa siku zile katika nchi hiyo. Ndipo, Aburamu alipomwambia Loti: Tusigombane mimi na wewe, wala wachungaji wangu na wachungaji wako! Kwani sisi tu ndugu. Huoni nchi yote iliyoko mbele yako? Na tutengane! Ukitaka kushotoni, nitakwenda kuumeni; ukitaka kuumeni, nitakwenda kushotoni. Loti akayainua macho yake, akaliona bonde zima la Yordani, ya kuwa lote lilikuwa lenye maji mengi kufika hata Soari; Bwana alipokuwa hajaiangamiza bado Sodomu na Gomora, lilikuwa kama shamba la Mungu, kama Misri. Kwa hiyo Loti akajichagulia hilo bonde zima la Yordani, kisha Loti akaondoka kwenda huo upande wa maawioni kwa jua. Hivyo ndivyo, hao ndugu walivyotengana. Aburamu akakaa katika nchi ya Kanaani, naye Loti akakaa katika miji ya hilo bonde, akaenda kuyapiga mahema yake mpaka Sodomu. Lakini watu wa Sodomu walikuwa wabaya, wakamkosea Bwana sana. Aburamu alipokwisha kutengana na Loti, Bwana akamwambia: Yainue macho yako, utazame toka mahali hapa, unapokaa, upande wa kaskazini na wa kusini na wa maawioni kwa jua na wa baharini! Nchi hizi zote, unazoziona, nitakupa wewe nao wa uzao wako kuwa zenu kale na kale. Nao wazao wako nitawafanya kuwa wengi kama mavumbi ya nchi. Kama mtu anaweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, wa uzao wako nao watahesabika. Inuka, utembee katika nchi hii kuuona urefu wake na upana wake! Kwani ndiyo, nitakayokupa wewe. Kisha Aburamu akayafunga mahema, akaenda kukaa katika kimwitu cha Mamure kilichokuwa karibu ya Heburoni, akajenga huko pa kumtambikia Bwana. Ikawa siku zile za Amurafeli, mfalme wa Sinari, ndipo, yeye na Arioki, mfalme wa Elasari, na Kedori-Laomeri, falme wa Elamu, na Tidali, mfalme wa Goyimu, wakaenda kupiga vita na Bera, mfalme wa Sodomu, na Birsa, mfalme wa Gomora na Sinabu, mfalme wa Adima, na Semeberi, mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela unaoitwa Soari. Hawa wote wakajiunga, wakakutana bondeni kwa Sidimu kwenye Bahari ya Chumvi. Kwani wale walimtumikia Kedori-Laomeri miaka kumi na miwili, lakini katika mwaka wa kumi na tatu walimvunjia maagano. Kwa hiyo Kedori-Laomeri na wafalme waliokuwa naye wakaja katika mwaka wa kumi na nne, wakawapiga wale Majitu kule Astaroti-Karnaimu nao Wazuzi kule Hamu nao Waemi katika nchi ya tambarare ya Kiriataimu, nao Wahori milimani kwao Seiri mpaka Eli-Parani ulioko upande wa nyikani. Kisha wakarudi, wakafika kwenye chemchemi ya Misipati, ndio Kadesi, wakaipiga nchi yote ya Waamaleki nao Waamori waliokaa Hasasoni-Tamari. Ndipo, walipotoka, mfalme wa Sodomu na mfalme wa Gomora na mfalme wa Adima na mfalme wa Seboimu na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakajipanga katika bonde la Sidimu kupigana. Nao wa Kedori-Laomeri, mfalme wa Elamu, na Tidali, mfalme wa Goyimu, na Amurafeli, mfalme wa Sinari, na Arioki, mfalme wa Elasari, walikuwa wafalme wanne, nao wale ni watano. Nako kule bondeni kwa Sidimu kulikuwa na mashimo mengi ya lami, nao wafalme wa Sodomu na wa Gomora walipokimbizwa wakatumbukia mlemle, nao watu waliosalia wakakimbilia milimani. Ndipo, walipoyateka mapato yote ya Sodomu na ya Gomora, navyo vilaji vyao vyote, wakaenda zao. Naye Loti, mwana wa nduguye Aburamu, wakamteka na mapato yake, wakenda zao, kwani alikaa Sodomu. Mtu mmoja aliyejiponya akaja, akamsimulia Mwebureo Aburamu yaliyokuwa; naye alikuwa akikaa katika kimwitu cha Mwamori Mamure aliyekuwa ndugu yao Eskoli na Aneri, nao hao walikuwa wamefanya maagano na Aburamu. Aburamu aliposikia, ya kuwa ndugu yake ametekwa, akawachukua wazalia wa nyumbani mwake 318 waliozijua kazi za vita, akapiga mbio akiwafuata mpaka Dani. Usiku akawagawanya watu wake, akawashambulia, akawapiga; kisha akawakimbiza mpaka Hoba ulioko kushotoni kwa Damasko. Akayarudisha yale mapato yote, naye ndugu yake Loti akamrudisha pamoja na mapato yake, nao wanawake wa watu waliotekwa. Aliporudi kwa kumpiga Kedori-Laomeri na wale wafalme waliokuwa naye, mfalme wa Sodomu akatoka kumwendea njiani kule bondeni kwa Sawe, ndio bondeni kwa Mfalme. Naye Melkisedeki, mfalme wa Salemu, akamotolea mkate na mvinyo, naye alikuwa mtambikaji wa Mungu alioko huko juu. Akambariki na kusema: Aburamu na atukuzwe kwa kuwa wake Mungu, mwenye mbingu naa nchi! Atukuzwe naye Mungu alioko huko juu, kwa kuwa amewatia adui zako mkononi mwako! Ndipo Aburamu alipompa fungu la kumi la mali zote, alizokuwa nazo. Kisha mfalme wa sodomu akamwambia Aburamu: Nipe watu wangu tu, mali uzitwae wewe. Lakini Aburamu akamwambia mfalme wa Sodomu: Mkono wangu namnyoshea Bwana Mungu alioko huko juu, aliye mwenye mbingu na nchi, kwamba: Katika mali zote zilizo zako sitachukua uzi wala kikanda tu cha kiatu, usiseme: Aburamu mali zake nyingi nimempa mimi. Hawa vijana tu wape chakula chao! Nao waume hawa waliokwenda pamoja nami, Aneri na Eskoli na Mamure, wao na wayachukue mafungu yao! Mambo hayo yalipomalizika neno la Bwana likamjia Aburamu katika ndoto kwamba: Usiogope Aburamu! Mimi ni ngao yako, nao mshahara wako ni mwingi. Aburamu akasema: Bwana Mungu, utanipa nini? Mimi ninajikalia pasipo mwana. Mwenye mali zilizomo nyumbani mwangu atakuwa huyu Eliezeri wa Damasko. Kisha Aburamu akasema: Hukunipa mzao; kwa hiyo atakayezichukua mali zangu ni mzalia wa nyumbani mwangu. Ndipo, neno la Bwama lilipomjia tena kwamba: Huyu hatazichukua mali zako; ila atakyetoka mwilini mwako ndiye atakayezichukua mali zako. Kisha akamtoa nje, akamwambia: Tazama juu mbinguni, uzihesabu nyota, kama unaweza kuzihesabu! Akamwambia: Hivi ndivyo, wao wa uzao wako watakavyokuwa wengi. Naye akamtegemea Bwana, kwa hiyo akamwazia kuwa mwenye wongofu. Kisha akamwambia: Mimi ni Bwana, nimekutoa kule Uri wa Wakasidi, nikupe nchi hii, uichukue kuwa yako. Naye akamwuliza: Bwana Mungu, nitajua namna gani, ya kuwa nitaichukua kuwa yangu? Akamwambia: Nipatie mori wa miaka mitatu na mbuzi jike wa miaka mitatu na dume la kondoo wa miaka mitatu na hua na kinda la njiwa! Alipokwisha kumpatia hao wote, akawapasua kati, akayaweka manusu ya kila nyama upande upande, yaelekeane, lakini ndege hakuwapasua. Ngusu walipoishukia ile mizoga, Aburamu akawaamia. Lakini jua lilipoingia, usingizi mzito ukampata Aburamu, mara akastushwa na giza kuu lililomguia. Ndipo, Bwana alipomwambia Aburamu: Na ujue kabisa, ya kuwa wao wa uzao wako watakaa ugenini katika nchi isiyo yao, nao watawatumikia wenyeji, hao watawatesa miaka 400. Nao wale wamizimu, ambao watawatumikia, mimi nitawahukumu, kisha wao watapata kutoka wenye mapato mengi. Lakini wewe utakwenda zako na kutengemana kwao baba zako, uzikwe utakapokwisha kuwa mzee wa miaka mingi. Nao watakaokuwa wa kizazi cha nne watarudi huku, kwa kuwa uovu wa Waamori haujatimia bado mpaka sasa. Jua lilipokwisha kuingia, kukawa na giza jeusi sana, mara likawa kama moshi wa tanuru wenye miali ya moto iliyopita katikati ya vile vipande vya nyama. Hivyo ndivyo, Bwana alivyofanya siku hiyo maagano na Aburamu kwamba: Nchi hii nitwapa wao wa uzao wako toka lile jito la Misri mpaka lile jito kubwa, lile jito la Furati, kwao Wakeni na Wakenizi na Wakadimoni, na Wahiti na Waperizi na wale Majitu, na Waamori na Wakanaani na Wagirgasi na Wayebusi. Sarai, mkewe Aburamu, hakumzalia mwana. Naye alikuwa na kijakazi wa Kimisri, jina lake Hagari. Kwa hiyo akamwambia Aburamu: Unaona, ya kuwa Bwana amenifunga, nisizae; sasa ingia kwa kijakazi wangu! Labda nitapata mlango kwake yeye. Aburamu akayaitikia, Sarai aliyoyasemaa. Kisha Sari, mkewe Aburamu, akamchukua Hagari, kijakazi wake wa Kimisri, akampa mumewe Aburamu kuwa mkewe, Aburamu naye alikuwa amekwisha kukaa miaka kumi katika nchi ya Kanaani. Alipoingia kwake Hagari, huyu akapata mimba; naye alipojiona kuwa mwenye mimba akambeua bibi yake, awe mdogo machoni pake. Ndipo, Sarai alipomwambia Aburamu: Mabaya ninayofanyiziwa na yakujie wewe! Mimi nimemweka kijakazi wangu kifuani pako; naye alipojiona kuwa mwenye mimba hunibeua, niwe mdogo machoni pake. Bwana na atuamulie mimi na wewe! Naye Aburamu akamwambia Sarai: Tazama, kijakazi wako yumo mkononi mwako! Mfanyizie yaliyo mema machoni pako! Lakini Sarai alipomnyenyekeza, akatoroka usoni pake. Malaika wa Bwana akamwona nyikani penye kisima cha maji, ndicho kisima kilichoko katika njia ya Suri. Akasema: Hagari, kijakazi wa Sarai, unatoka wapi? Tena unakwenda wapi? Akasema: Nimetoroka, nitoke usoni pake bibi yangu Sarai. Ndipo, malaika wa Bwana alipomwambia: Rudi kwa bibi yako na kuunyenyekea mkono wake! Malaika wa Bwana akamwambia tena: Wao wa uzao wako nitawafanya kuwa wengi, wasihesabike kwa wingi. Malaika wa Bwana akaendelea kumwambia: Ninakuona kuwa mwenye mimba. Mwana, utakayemzaa, mwite jina lake Isimaeli (Mungu husikia), kwa kuwa Bwana amekusikia, ulipomlalamikia kwa kuteseka. Naye atakuwa mwenye ukali kama punda wa porini, mkono wake utawapingia watu wote, nayo mikono yao wote itampingia yeye, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote. Ndipo, alipomwita Bwana aliyesema naye jina lake: Wewe Mungu unaniona, kwani alisema: Kumbe nami nimemwona, aliponitazama. Kwa hiyo kile kisima watu hukiita Kisima cha Mwenye Uzima Anionaye, nacho kiko katikati ya Kadesi na Beredi. Kisha Hagari akamzalia Aburamu mtoto mume, naye Aburamu akamwita huyu mwana, Hagari aliyemzaa, jina lake Isimaeli. Naye Aburamu alikuwa mwenye miaka 86, Hagari alipomzalia Aburamu huyu Isimaeli. Aburamu alipokuwa mwenye miaka 99, Bwana akamtokea Aburamu, akamwambia: Mimi ni Mungu Mwenyezi, uendelee machoni pangu na kunicha! Hivyo tutaagana sote wawili, mimi na wewe, nami nitakufanya kuwa watu wengi sanasana. Ndipo, Aburamu alipomwangukia usoni pake, naye Mungu akaendelea kusema naye kwamba: Tazama! Nina agano na wewe, uwe baba yao mataifa mazima ya watu. Kwa hiyo usiitwe tena jina lako Aburamu (Baba mtukufu), ila jina lako liwe Aburahamu (Baba yao wengi)! Kwani nimekuweka kuwa baba yao mataifa mengi ya watu. Nitakupa wazao wengi sanasana, nikufanye kuwa mataifa, nao wafalme watatoka kwako. Nitalisimamisha agano langu, tuliloliagana mimi na wewe nao wa uzao wako wajao nyuma yako, liwe agano la vizazi vya kale na kale, niwe Mungu wako na Mungu wao wa uzao wako wajao nyuma yako. Nitakupa wewe nao wa uzao wako wajao nyuma yako nchi hii, unayoikaa ugeni, ndiyo nchi yote ya Kanaani, mwichukue, iwe yenu kale na kale, nami nitakuwa Mungu wao. Kisha Mungu akamwambia Aburahamu: Liangalieni Agano langu, wewe nao wa uzao wako wajao nyuma yako, vizazi kwa vizazi! Nalo hili ndilo Agano langu la kuliangalia, tunaloliagana mimi na wewe nao wa uzao wako wajao nyuma yako: Kwenu sharti atahiriwe kila aliye wa kiume. Mkizikata nyama za magovi yenu, hii itakuwa kielekezo cha Agano, tuliloliagana mimi nanyi. Kwenu kila mtoto wa kiume aliye wa vizazi vyenu akimaliza siku nane sharti atahiriwe. Vivyo hivyo nao wazalia wa nyumbani nao wasio wa uzao wako walionunuliwa kwa fedha kwa wageni wo wote. Hao wazaliwa nyumbani mwako nao walionunuliwa kwa fedha zako sharti nao watahiriwe. Hili Agano langu la kuzikata hizo nyama za miili yenu sharti liwe la kale na kale. Kwa hiyo mtu mume mwenye govi asiyekatwa nyama ya govi lake sharti roho yake yeye ing'olewe, atoweke kwao walio wa ukoo wake, maana ni mwenye kulivunja Agano langu. Kisha Mungu akamwambia Aburahamu: Mkeo Sarai asiitwe tena jina lake Sarai, ila jina lake liwe Sara (Mama mkuu)! Kwani nitambariki, nikupatie kwake mtoto mume; nitakapombariki, atakuwa mama wa mataifa mazima, nao wafalme wa makabila ya watu watatoka kwake. Ndipo, Aburahamu alipomwangukia usoni pake, akacheka na kusema moyoni mwake: Itawezekanaje, mwenye miaka mia azaliwe mtoto? Huyu Sara aliye mwenye miaka 90 atazaaje? Kwa hiyo Aburahamu akamwambia Mungu: Afadhali Isimaeli angepata kuwapo machoni pako! Ndipo, Mungu aliposema: Ni kweli, mkeo Sara atakuzalia mtoto mume, nalo jina lake uliite Isaka (Acheka); naye ndiye, nitakayemsimamishia Agano langu kuwa la kale na kale kwao wa uzao wake wajao nyuma yake. Hata kwa ajili ya Isimaeli nimekusikia: Tazama, nitambariki naye na kumpa wazao wengi na kumfanya kuwa wengi sanasana, atazaa wakuu 12, nami nitamfanya kuwa taifa kubwa. Lakini lile Agano langu nitamsimamishia Isaka, Sara atakayekuzalia siku zizi hizi za mwaka ujao. Mungu alipokwisha kusema naye, akapaa juu na kutoka kwake Aburahamu. Kisha Aburahamu akamchukua mwanawe Isimaeli nao wazaliwa wote wa nyumbani mwake nao wote, aliowanunua kwa fedha zake, watu waume wote pia waliokuwamo nyumbani mwake Aburahamu, akawakata nyama za magovi yao siku iyo hiyo, kama Mungu alivyomwambia. Aburahamu alikuwa mwenye miaka 99 alipokatwa nyama ya govi lake. Naye mwanawe Isimaeli alikuwa mwenye miaka 13 alipokatwa nyama ya govi lake. Siku iyo hiyo moja Aburahamu na mwanawe isimaeli walitahiriwa. Nao waume wote wa nyumbani mwake, wazalia wa nyumbani nao, aliowanunua kwa fedha kwa watu wasio wa kabila lake, wote walitahiriwa pamoja naye. Kisha Bwana akamtokea katika kimwitu cha Mamure, mwenyewe alipokuwa amekaa hapo pa kuingia hemani kwa kuwa jua kali. Alipoyainua macho yake akaona watu watatu, wakisimama hapo, alipo; alipowaona akawapigia mbio na kuondoka hapo pa kuingia hemani, akawainamia chini, akawaambia: Bwana wangu, kama nimeona mapendeleo machoni pako, usipite penye mtumishi wako! Mtaletewa maji kidogo ya kuiosha miguu yenu, kisha mtapumzika chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mioyo yenu ipate kutulia, kisha mtakwenda zenu, kwani huku, mnakopita, ni kwake mtuma wenu. Nao wakamwambia: Fanya, kama ulivyosema! Aburahamu akaingia upesi hemani kwa Sara, akamwambia: Chukua upesi pishi sita za unga mwembamba uliochungwa vema, uukande, utengeneze mikate! Kisha Aburahamu akapiga mbio kwenda kwenye ng'ombe, akachukua ndama mwanana mwenye nyama nzuri, akampa kijana, naye akaenda kuitengeneza vizuri. Kisha Aburahamu akawaandalia siagi na maziwa na nyama za ndama, yule alizozitengeneza, nao wakala, mwenyewe akisimama karibu yao chini ya mti. Kisha wakamwuliza: Mkeo Sara yuko wapi? Akajibu: Yumo hemani. Akamwambia: Nitakaporudi kwako siku zizi hizi za mwaka ujao, ndipo, mkeo Sara atakapokuwa mwenye mtoto wa kiume. Naye Sara aliyasikia, maana alikuwa nyuma yake hapo pa kuingia hemani. Lakini Aburahamu na Sara walikuwa wazee wenye siku nyingi, naye Sara alikuwa amekoma kupatwa na yale mambo ya kike. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake kwamba: Hivyo, nguvu za mwili wangu zilivyokwisha kupotea, nitawezaje kuipata hiyo furaha? Tena bwana wangu naye ni mzee. Ndipo, Bwana alipomwambia Aburahamu: Mbona Sara anacheka kwamba: Kumbe mimi nitazaa kweli, nami ni mzee? Je? Liko jambo linalomshinda Bwana? Wakati, nitakaporudi kwako, siku zizi hizi za mwaka ujao ndipo, Sara atakapokuwa mwenye mtoto wa kiume. Lakini Sara akakana kwamba: Sikucheka, kwani aliogopa; naye akasema: Sivyo, umecheka. Kisha wale waume wakaondoka huko, wakajielekeza kwenda Sodomu, naye Aburahamu akaenda nao, awasindikize. Bwana akasema: Nitamfichaje Aburahamu ninayotaka kuyafanya? Maana Aburahamu atakuwa taifa kubwa lenye nguvu, namo mwake ndimo, mataifa yote ya nchini yatakamobarikiwa. Kwani ninamjua, ya kuwa atawaagiza wanawe nao wa mlango wake wajao nyuma yake, waishike njia ya Bwana na kufanya yaongokayo nayo ya kweli, Bwana apate kumtimizia Aburahamu aliyomwagia. Kwa hiyo Bwana akasema: Makelele ya Sodomu na ya Gomora ni mengi, nayo makosa yao ni mazito mno. Nimeshuka, nitazame, kama hayo yote, ambayo niliyasikia makelele yao, wameyafanya kweli, au kama hawakuyafanya, nijue. Kisha wale watu wakageuka hapo kwenda Sodomu, lakini aburahamu akasalia hapo akisimama mbele ya Bwana. Aburahamu akafika karibu, akauliza: Utamwondoa mwongofu pamoja naye asiyekucha? Labda mle mjini wamo waongofu 50; basi, utawaondoa nao? Hutapahurumia mahali hapo kwa ajili ya waongofu 50 waliopo? Jambo kama hilo halipasi kabisa, ulifanye, ukimwua mwongofu pamoja naye asiyekucha, mwongofu akiwa kwako kama mwingine asiyekucha. Hili halikupasi kabisa wewe utakayewaamua walimwengu wote, hayo si maamuzi, utakayoyaamua. Bwana akasema: Kama nitawaona waongofu 50 mle mjini mwa Sodomu, nitapahurumia mahali pale pote kwa ajili yao. Aburahamu akajibu kwamba: Tazama nimejipa moyo wa kusema na Bwana, ingawa mimi ni mavumbi na majivu. Labda wale waongofu 50 wamepunguka watano, sasa utaungamiza mji wote kwa ajili ya hao watano? Akasema: Sitauangamiza, kama nitaona humo 45. Akaendelea kusema naye kwamba: Labda wataonekana humo 40 tu. Akasema: Sitafanya kitu kwa ajili yao hao 40. Akasema: Makali ya Bwana yasiwake moto, nikisema tena: Labda wataonekana humo 30 tu. Akasema: Sitafanya kitu, kama nitaona humo 30 tu. Akasema: Tazama, nimejipa moyo wa kusema na Bwana: Labda wataonekana humo 20 tu. Akasema: Sitauangamiza kwa ajili yao hao 20. Akasema: Makali ya Bwana yasiwake moto, nikisema tena mara moja tu: Labda wataonekana humo 10 tu. Akasema: Sitauangamiza kwa ajili yao hao 10 tu. Bwana alipokwisha kusema na Aburahamu akaenda zake, naye Aburahamu akarudi mahali pake. Ilipokuwa jioni, wale malaika wawili wakafika Sodomu, naye Loti alikuwa amekaa langoni huko Sodomu. Alipowaona Loti akainuka kuwaendea njiani, akawaangukia usoni chini, akawaambia: Mabwana, njoni kufikia nyumbani mwa mtumwa wenu, mlale, mwioshe miguu yenu! Kesho mtaondoka na mapema kwenda zenu; lakini wakakataa wakisema: Tutalala nje. Ndipo, alipowahimiza sana, mpaka wakifikia kwake; walipoingia nyumbani mwake, akawatengenezea cha kunywa, akachoma mikate isiyochachwa, nao wakala. Walipokuwa hawajalala bado, watu wa ule mji wa Sodomu, vijana kwa wazee, watu wote waliotoka pande zote wakaja, wakaizunguka hiyo nyumba, wakamwita Loti, wakamwuliza: Wako wapi wale waume waliokuja kwako usiku huu? Walete, watutokee, tupate kuwajua! Loti akawatokea hapo pa kuingilia na kuufunga mlango nyuma yake, akasema: Ndugu zangu, msifanye mabaya! Tazameni! Ninao wanangu wa kike wawili wasiojua bado mtu mume, nitawatoa, niwape ninyi, mwafanyizie yaliyo mema machoni penu; lakini waume hao msiwafanyizie neno, kwani kwa sababu hii wmeingia kivulini mwa kipaa changu. Wakasema: Ondoka hapa! Tena wakaambiana: Ni mgeni peke yake kwetu, tena anataka kutuamua. Wakamsonga sana huyu Loti wakitaka kuukaribia mlango, wauvunje. Ndipo, wale watu walipoitoa mikono yao, wakamwingiza Loti kwao nyumbani, kisha wakaufunga mlango. Lakini wale watu waliokuwa nje hapo pa kuingia nyumbani wakawapofusha macho, wadogo kwa wakubwa, wakashindwa kupaona hapo pa kuingia nyumbani. Kisha wale waume wakamwambia Loti: Kama unao ndugu, wakweo na wanao wa kiume na wa kike nao wo wote walio wako humu mjini, wachukue, utoke nao mahali hapa! Kwani sisi tutapaangamiza mahali hapa; kwani makelele yao ni makubwa masikioni mwake Bwana, kwa hiyo Bwana ametutuma, tupaangamize. Loti alipotoka kusema na wakwewe waliowaoa wanawe wa kike, akawaambia: Inukeni, mtoke mahali hapa! Kwani Bwana ataungamiza mji huu. Lakini machoni pao wakwewe alikuwa kama mtu anayetaka kuwachekesha tu. Kulipopambazuka, wale malaika wakamhimiza Loti kwamba: Ondoka! Mchukue mkeo nao wanao wawili wa kike, ulio nao, usiuawe nawe kwa ajili ya manza za mji huu! Alipozuzuika, wale waume wakawashika mikono, yeye na mkewe na wanawe, kwa huruma, Bwana alizowapatia, wakawatoa mjini na kuwapeleka nje. Walipokwisha kuwatoa na kuwapeleka nje, akasema: Iponye roho yako! Usitazame nyuma, wala usisimame huku bondeni mahali pawapo pote, ila kimbilia milimani, usiuawe! Loti akawaambia: Usiseme hivyo, Bwana wangu! Kwa kuwa mtumwa wako aliona upendeleo machoni pako, ukazizidisha huruma zako, ulizonifanyia, uiponye roho yangu! Tazama, sitaweza kukimbilia milimani kwa kwamba: Yale mabaya yatanipata, nami nitakufa. Tazama, huko karibu uko mji wa kuukimbilia, nao ni mdogo; acha, niukimbilie huo, kwa kuwa mdogo, niiponye roho yangu! Naye akamwambia: Basi, hata katika neno hili nitakuitikia, nisiufudikize nao mji huo, uliousema. Jihimize kuukimbilia! Kwani siwezi kufanya lo lote, mpaka ufike humo. Kwa hiyo wakaliita jina la mji huo Soari (Mdogo). Loti alipoingia Soari, jua lilikuwa linachomoza. Ndipo, Bwana aliponyesha mvua ya moto uliochanganyika na mawe ya kiberitiberiti kwenye miji ya Sodomu na Gomora; mvua hii ilitoka kwake Bwana mbinguni. Ndivyo, Mungu alivyoifudikiza hiyo miji nalo hilo bonde lote pamoja na watu waliokaa humo mijini nayo majani yote yaliyochipuka katika nchi ile. Naye mkewe Loti alipoyatazama ya nyuma akawa nguzo ya chumvi. Kesho yake Aburahamu akaamka na mapema kwenda pale, aliposimama mbele ya Bwana. Akachungulia upande wa Sodomu na Gomora na upande wa nchi zote za bonde hilo, mara akaona, moshi ulivyopanda kutoka chini kama moshi wa tanuru. Lakini hapo, Mungu alipoiangamiza miji ya lile bonde, Mungu alimkumbuka Aburahamu, amtoe Loti katika mafudikizo hayo na kumpeleka pengine alipoifudikiza hiyo miji, Loti alimokuwa na kukaa humo. Kisha Loti akatoka Soari, akapanda milimani kukaa huko pamoja na wanawe wawili wa kike, kwani aliogopa kukaa mle Soari; kwa hiyo akakaa pangoni yeye pamoja na wanawe wawili. Kisha yule wa kwanza akamwambia mdogo wake: Baba yetu ni mzee, tena hakuna mtu mume katika nchi hii yote wa kuingia kwetu, kama ilivyo desturi po pote duniani. Haya! Na tumlevye baba yetu kwa mvinyo, kisha tulale naye, tupate kwa baba yetu mimba za kuukalisha mlango! Basi, wakamlevya baba yao usiku huo, kisha yule mkubwa akaingia kwa baba yake, akalala naye, lakini mwenyewe hakujua, alipokuja kulala naye, wala alipoondoka. Kesho yake yule mkubwa akamwambia mdogo wake: Tazama, usiku wa jana nimelala na baba yangu; haya! Na tumlevye kwa mvinyo hata siku ya leo, upate kuingia kwake na kulala naye, tupate kwa baba yetu mimba za kuukalisha mlango! Kisha wakamlevya baba yao kwa mvinyo nao usiku huo, naye mdogo akaingia, akalala naye, lakini mwenyewe hakujua, alipokuja kulala naye, wala alipoondoka. Hivyo ndivyo, wana wa kike wa Loti wote wawili walivyopata mimba kwa baba yao. Yule mkubwa alipozaa mtoto mume akamwita jina lake Moabu (Wa baba), naye ni baba yao Wamoabu mpaka leo. Yule mdogo alipozaa mtoto mume akamwita jina lake Ben-Ami (Mwana wa Kwetu), naye ni baba yao wana wa Amoni mpaka leo. Kisha aburahamu akaondoka huko kwenda katika nchi ya upande wa kusini, akakaa ugenini katikati ya Kadesi na Suri huko Gerari. Kwa ajili ya mkewe Sara Aburahamu akasema: Huyu ni dada yangu. Kwa hiyo Abimeleki, mfalme wa Gerari, akatuma watu kumchukua Sara. Ndipo, Mungu alipokuja kwa mfalme Abimeleki usiku katika ndoto, akamwambia: Tazama, utakufa kwa ajili ya huyu mwanamke, uliyemchukua, maana ni mke wa bwana mwingine. Naye Abimeleki alikuwa hajamkaribia bado, kwa hiyo akasema: Bwana, watu wasiokosa utawaua nao? Yule hakuniambia: Huyu ni dada yangu? Naye mwenyewe amesema: Yule ni kaka yangu. Hivyo nimevifanya kwa moyo usiojua kuwa vibaya na kwa mikono iliyotakata. Ndipo, Mungu alipomwambia katika ndoto: Mimi nami nimejua, ya kama umevifanya hivyo kwa moyo usiovijua kuwa vibaya. Kwa sababu hii mimi nami nimekuzuia, usinikosee, nikakukataza kumgusa. Sasa mrudishie yule mtu mkewe! Kwani ni mfumbuaji, akuombee, upate kupona; lakini usipomrudisha, ujue, ya kuwa utakufa kweli, wewe pamoja nao wote walio wako. Kesho yake abimeleki akaamka na mapema, akawaita watumishi wake wote, akayasema hayo maneno yote masikioni pao; ndipo, hao watu waliposhikwa na woga kabisa. Kisha Abimeleki akamwita Aburahamu, akamwambia: Kwa nini umetufanyia hivyo? Mimi nimekukosea nini, ukitaka kunikosesha sana mimi pamoja nao, ninaowatawala? Umenifanyizia mambo yasiyofanywa. Abimeleki akamwuliza Aburahamu: Umeona nini ukilifanya jambo hilo? Aburahamu akasema: Nimesema tu moyoni: Huku hakuna wenye kumwogopa Mungu, kwa hiyo wataniua kwa ajili ya mke wangu. Naye ni dada yangu kweli kwa kuwa mwana wa baba yangu, lakini si mwana wa mama yangu, kwa hiyo aliweza kuwa mke wangu. Ikawa hapo, Mungu aliponitoa nyumbani mwa baba yangu kusafiri huku na huko, nikamwambia: Unifanyie upendeleo huu, po pote tutakapofika, useme kwa ajili yangu: Huyu ni kaka yangu. Ndipo, Abimeleki alipochukua mbuzi na kondoo na ng'ombe na watumwa wa kiume na wa kike, akampa Aburahamu, akamrudishia mkewe Sara, akamwambia: Tazama, nchi yangu iko mbele yako, kaa palipo pema machoni pako! Naye Sara akamwambia: Tazama, kaka yako nimempa fedha elfu, upate kaya za kuwafunika ushungi wao wote, ulio nao; ndivyo, utakavyojulikana kwao wote kuwa mtu asiyekosa. Aburahamu alipomwomba Mungu, Mungu akamponya Abimeleki, naye mkewe, nao vijakazi wake, wakapata kuzaa tena. Kwani Bwana alikuwa ameyakomesha kuzaa matumbo yao wote wa mlango wa Abimeleki kwa ajili ya Sara, mkewe Aburahamu. Bwana akamkagua Sara, kama alivyosema; naye Bwana akamfanyizia Sara, kama alivyomwagia. Kwa hiyo Sara akapata mimba, akamzalia Aburahamu mtoto mume katika uzee wake siku zizo hizo, Mungu alizomwagia. Mwanawe aliyezaliwa, Sara aliyemzaa, Aburahamu akamwita jina lake Isaka (Acheka). Huyu mwanawe aburahamu akamtahiri, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwagiza. Naye Aburahamu alikuwa mwenye miaka 100, mwanawe Isaka alipozaliwa. Naye Sara akasema: Mungu amenipatia kuchekwa, kwani kila atakayevisikia atanicheka. Akasema tena: Yuko nani aliyemwambia Aburahamu: Sara atanyonyesha wana? Kwani nimezaa mwana katika uzee wake. Mtoto alipokua akakomeshwa kunyonya; siku hiyo, Isaka alipoacha kunyonya, Aburahamu akafanya karamu kubwa. Sara alipomwona yule mwana wa Mmisri Hagari, aliyemzalia Aburahamu kuwa mfyozaji, Akamwambia Aburahamu: Mfukuze huyu kijakazi pamoja na mwanawe! Kwani mwana wa huyu kijakazi hatapata urithi pamoja na mwanangu Isaka. Neno hili likawa baya sana machoni pake Aburahamu kwa ajili ya mwanawe, lakini Mungu akamwambia Aburahamu: Neno hilo lisiwe baya machoni pako kwa ajili ya huyo kijana na huyo kijakazi wako! Yote, Sara atakayokuambia, mwitikie sauti yake! Kwani watakaoitwa uzao wako ni wa Isaka tu. Lakini mwana wa kijakazi naye nitamweka kuwa taifa zima, kwani naye ni uzao wako. Kesho yake Aburahamu akaamka na mapema, akachukua mkate na kibuyu cha maji, akampagaza Hagari begani, kisha akampa na mwanawe; ndivyo, alivyompa ruhusa kwenda zake. Lakini alipokwenda akapotea katika nyika ya Beri-Seba. Maji yalipokwisha kibuyuni, akamwacha mwanawe chini ya kijiti, akaenda kukaa peke yake na kumwelekea mbali kidogo kama hapo, mtu anapotupa mshale kwa upindi, kwani alisema: Nisione, mwana anavyokufa! Alipokaa hivyo na kumwelekea akapaza sauti yake, akalia. Mungu alipokisikia kilio cha mtoto, malaika wa Mungu akamwita Hagari toka mbinguni, akamwambia: Una nini, Hagari? Usiogope! Kwani Mungu amekisikia kilio cha mtoto hapo, anapolala. Inuka, umwinue mtoto na kumshika kwa mkono wako! Kwani nitamfanya kuwa taifa kubwa. Kisha Mungu akamfumbua macho; ndipo, alipoona kisima cha maji, akaenda kukijaza kile kibuyu, akampa mtoto, anywe. Mungu akawa na huyu mtoto, akakua, akakaa nyikani, akawa mpiga upindi. Akakaa katika nyika ya Parani; naye mama yake akamwoza mwanamke wa nchi ya Misri. Ikawa wakati huo, ndipo, Abimeleki na Pikoli, mkuu wa vikosi vyake, walipomwambia Aburahamu kwamba: Mungu yuko pamoja na wewe katika mambo yote, unayoyafanya. Sasa niapie na kumtaja Mungu kwamba: Hutanidanganya mimi wala wao wa uzao wangu wajao nyuma yangu, ila huo wema, niliokufanyia wewe, unifanyie mimi nayo nchi hii, unayoikaa ugeni! Aburahamu akasema: Basi, mimi nitaapa. Kisha Aburahamu akamwonya Abimeleki kwa ajili ya kisima cha maji, watumishi wake Abimeleki walichokinyang'anya. Naye Abimeleki akasema: Simjui aliyelifanya jambo hilo, wewe nawe hujanipasha habari, mimi nami sijavisikia, ni leo hivi tu. Kisha Aburahamu akachukua mbuzi na kondoo na ng'ombe, akampa Abimeleki; hivyo ndivyo, wao wawili walivyofanya agano. Aburahamu akaweka wana kondoo saba peke yao, naye Abimeleki akamwuliza Aburahamu: Hawa wana kondoo saba ukiwaweka peke yao, ni wa nini? Akajibu: Hawa wana kondoo saba wa kike wachukue mkononi mwangu, upate kunishuhudia, ya kuwa nilikichimbua kisima hiki. Kwa sababu hii wakapaita mahali pale Beri-Seba (Kisima cha Kiapo), kwa kuwa waliapiana hapo wote wawili. Walipokwisha kulifanya agano hilo hapo Beri-Seba, Abimeleki na Pikoli, mkuu wa vikosi vyake, wakaondoka, wakarudi katika nchi ya Wafilisti. Aburahamu akapanda mvinje hapo Beri-Seba, akalitambikia hapo Jina la Bwana aliye Mungu wa kale na kale. Aburahamu akakaa ugenini katika nchi ya Wafilisti siku nyingi. Ikawa, mambo hayo yalipomalizika, Mungu akamjaribu Aburahamu, akamwambia: Aburahamu! naye akajibu: Mimi hapa! Akamwambia: Mchukue mwana wako wa pekee, umpendaye, huyo Isaka, uende naye katika nchi ya Moria, umtoe huko kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima juu ya mlima mmoja, nitakaokuonyesha! Basi, kesho yake Aburahamu akaamka na mapema, akamtandika punda wake, akachukua na vijana wawili kwenda naye, tena mwanawe Isaka; alipokwisha kuchanja nazo kuni za kuchomea ng'ombe ya tambiko, akaondoka kwenda mahali pale, Mungu alipomwambia. Aburahamu alipoyainua macho yake siku ya tatu akapaona mahali pale, pangaliko mbali. Ndipo, Aburahamu alipowaambia wale vijana wake: Kaeni hapa pamoja na punda! Mimi na huyu kijana tutakwenda huko kutambika, kisha tutarudi kwenu. Aburahamu akazichukua zile kuni za kuchomea ng'ombe ya tambiko, akamtwika mwanawe Isaka, naye mwenyewe akashika moto na kisu mkononi mwake, wakaenda hivyo wao wawili pamoja. Isaka akamwmbia baba yake Aburahamu: Baba! Akajibu: Mimi hapa, mwanangu! Akasema: Tazama! Moto na kuni tunazo, lakini mwana kondoo wa kuwa ng'ombe ya tambiko yuko wapi? Aburahamu akasema: Mwanangu, Mungu atajipatia mwana kondoo wa kuwa ng'ombe ya tambiko. Kisha wakaenda hivyo wao wawili pamoja. Walipofika mahali pale, Mungu alipomwambia, Aburahamu akajenga hapo pa kutambikia, akazitandika kuni juu yake; kisha akamfunga mwanawe Isaka, akamweka hapo pa kutambikia juu ya hizo kuni; kisha Aburahamu akaukunjua mkono wake, akakishika kisu cha kumchinjia mwanawe. Ndipo, malaika wa Bwana alipomwita toka mbinguni kwamba: Aburahamu! Aburahamu! Akaitikia: Mimi hapa! Akamwambia: Usimkunjulie mtoto mkono wako! Usimfanyizie cho chote! Kwani sasa nimejua, ya kuwa unamwogopa Mungu, maana hukumnyima hata mwanao wa pekee. Aburahamu alipoyainua macho yake akaona kulungu nyuma yake aliyekamatwa pembe zake na kichaka; huyo kulungu akamtumia kuwa ng'ombe ya tambiko mahali pake mwanawe. Aburahamu akapaita mahali hapo: Bwana aona; kwa hiyo watu husema hata leo: Mlimani, Bwana anakoonwa. Malaika wa Bwana akamwita Aburahamu toka mbinguni mara ya pili, akasema: Ndivyo, asemavyo Bwana: Nimejiapia kwamba: Kwa kuwa umelifanya jambo hili, usininyime mwanao wa pekee, nitakubariki kweli, nikupe, uzao wako uwe watu wengi sana kama nyota za mbinguni au kama mchanga ulioko ufukoni kwenye bahari, hao wa uzao wako wayatwae malango ya adui zao kuwa yao. Katika uzao wako ndimo, mataifa yote ya nchini yatakamobarikiwa, kwa kuwa umeisikia sauti yangu. Kisha Aburahamu akarudi kwa wale vijana wake, wakaondoka, wakaenda zao pamoja kwenda Beri-Seba; kule Beri-Seba ndiko, Aburahamu alikokaa. Mambo hayo yalipomalizika, Aburahamu akapashwa habari kwamba: Tazama, naye Milka amemzalia ndugu yako Nahori wana. Mwanawe wa kwanza ni Usi, ndugu yake ni Buzi, tena Kemueli, baba yao Washami, na Kesedi na Hazo na Pildasi na Idilafu na Betueli. Naye Betueli akamzaa Rebeka. Milka alimzalia ndugu yake Aburahamu hao wanane, naye suria yake aliyeitwa Ruma akamzaa Teba, tena Gahamu na Tahasi na Maka. Siku zake Sara za kuwapo zilipopata miaka 127, hii miaka ya kuwapo kwake ilipotimia, Sara akafa huko Kiriati-Arba, ndio Heburoni, katika nchi ya Kanaani; ndipo, Aburahamu alipoingia nyumbani kumwombolezea na kumlilia. Kisha Aburahamu akaondoka kwa mfu wake, akasema na wana wa Hiti kwamba: Mimi ni mgeni anayejikalia tu kwenu, nipeni kwenu mahali pa kaburi, pawe pangu, nipate kumzika mfu wangu aliomo nyumbani kwangu! Nao wana wa Hiti wakamjibu Aburahamu kwamba: Tusikie, bwana wetu! Wewe u mkuu wa Mungu kwetu; mzike mfu wako katika kaburi lo lote la kwetu, utakalolichagua! Hakuna mtu wa kwetu atakayekunyima kaburi lake, kwamba usimzike mfu wako humo. Ndipo, Aburahamu alipoinuka, akawainamia watu wa nchi hii, wao wana wa Hiti, akasema nao kwamba: Roho zenu zikiitikia kwamba: Nimzike mfu wangu aliomo nyumbani mwangu, nisikilizeni, mniombee kwa Efuroni, mwana wa Sohari, anipe lile pango lake la Makipela lililoko penye mwisho wa shamba lake! Akinipa, nitamlipa katikati yenu fedha zote pia za kulinunua, liwe mahali pangu mimi pa kuzikia. Naye Efuroni alikuwa amekaa papo hapo katikati ya wana wa Hiti; ndipo, huyu Mhiti Efuroni alipomjibu Aburahamu masikioni pao Wahiti wote waliokuja hapo langoni penye mji wake kwamba: Sivyo, bwana wangu. Nisikie! Hilo shamba ninakupa, nalo pango lililomo ninakupa, machoni pao hawa wana wa ukoo wangu ninakupa, upate kumzika mfu wako. Ndipo, Aburahamu alipowainamia tena watu wa nchi hii, akamwambia Efuroni masikioni pa watu wa nchi hii kwamba: Ungenisikia tu! Chukua kwangu hizi fedha za kulinunua shamba hilo, nitakazokupa, nipate kumzika mfu wangu huko! Efuroni akamjibu Aburahamu kwamba: Bwana wangu, nisikie tu! Shamba la fedha 400 ni kitu gani, tubishane mimi na wewe? Mzike tu mfu wako! Aburahamu akamwitikia Efuroni; kwa hiyo Aburahamu akampimia Efuroni hizo fedha, alizozisema masikioni pao wana wa Hiti, fedha 400, wachuuzi walizozitumia, ndio shilingi 1600. Basi, shamba la Efuroni lililokuwa huko Makipela mbele ya Mamure, hilo shamba lenyewe pamoja na lile pango lililokuwako, nayo miti yote ya hapo shambani iliyokuwako mipakani katika mipaka yake ya pande zote, yote pamoja yakawa mali yake Aburahamu machoni pao wana wa Hiti wote waliokuja langoni penye mji wake. Baadaye Aburahamu akamzika mkewe Sara katika hilo pango la shamba la Makipela lililoko mbele ya Mamure, ndio Heburoni, katika nchi ya Kanaani. Ndivyo, hilo shamba pamoja na hilo pango lililoko lilivyotolewa kuwa mali yake Aburahamu, liwe mahali pake yeye pa kuzikia, likikoma kuwa lao wana wa Hiti. Aburahamu alikuwa mkongwe mwenye siku nyingi, nyingi sana, naye Bwana alikuwa amembariki Aburahamu po pote. Ndipo, Aburahamu alipomwambia mtumishi wake aliyepata uzee nyumbani mwake, aliyezitunza mali zake zote: Uweke mkono wako chini ya kiuno changu, nikuapishe kwake Bwana aliye Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi kwamba: Usimposee mwanangu mwanamke miongoni mwa wana wa kike wa Wakanaani, ambao ninakaa katikati yao! Ila uende katika nchi, nilikozaliwa, kwenye ndugu zangu kumposea mwanangu Isaka mkewe. Huyu mtumishi akajibu: Kama yule mwanamke hataki kunifuata kuja katika nchi hii, nimrudishe mwanao katika nchi ile, ulikotoka? Aburahamu akamwambia: Angalia sana, usimrudishe mwanangu kwenda huko! Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani mwa baba yangu na katika nchi, nilikozaliwa, aliniambia na kuniapia kwamba: Wa uzao wako ndio, nitakaowapa nchi hii. Yeye atatuma malaika wake, akutangulie, umpatie mwanangu mke huko. Lakini yule mwanamke asipotaka kukufuata, basi, utakuwa umefunguliwa, nacho hiki kiapo, ninachokutakia, kitakuwa kimetanguka, lakini usimrudishe mwanangu kwenda huko! Ndipo, yule mtumishi alipouweka mkono wake chini ya kiuno cha bwana wake Aburahamu, akamwapia kufanya hivyo. Kisha yule mtumishi akachukua ngamia kumi za bwana wake kwenda safari, akachukua navyo vitu vizuri vyote vya bwana wake, kisha akaondoka, akaenda Mesopotamia kwenye mji wa Nahori. Huko nje ya mji kwenye kisima cha maji akawapumzisha ngamia; ikawa jioni, wanawake watokapo kuchota maji. Akaomba kwamba: Bwana, Mungu wa bwana wangu Aburahamu, nipe kufanikiwa leo! Naye Bwana wangu Aburahamu mhurumie! Tazama, ninasimama hapa penye kisima cha maji, nao vijana wa kike wa watu wa humu mjini wanatoka kuchota maji. Nitakapomwambia kijana mmoja: Utue mtungi wako, ninywe! naye akisema: Haya! Unywe! Tena ngamia wako nao nitawanywesha, basi, awe yye, uliyemchagulia mtumishi wako Isaka! Nami ndipo, nitakapojua, ya kuwa umemhurumia bwana wangu. Alipokuwa hajaisha bado kuomba, mara akatokea Rebeka, binti Betueli aliyekuwa mwana wa Milka, mkewe Nahori, nduguye Aburahamu; naye alichukua mtungi begani. Huyu kijana wa kike alikuwa mzuri sana wa kumtazama, tena alikuwa angali mwanamwali asiyejua mtu mume bado. Huyu akaja kushuka kisimani, napo alipokwisha kuujaza mtungi wake akapanda. Ndipo, yule mtumishi alipomkimbilia, akasema: Nipe maji kodogo ya mtungini mwako, ninywe! Naye akasema: Haya! Unywe, bwanangu! Akaushusha upesi mtungi wake mkononi mwake, akampa, anywe. Alipokwisha kumnywesha, akasema: Ngamia wako nao nitawachotea, hata wamalize kunywa. Akamwaga upesi maji ya mtungini ndani ya birika, akapiga mbio kwenda kisimani tena kuchota; ndivyo, alivyowachotea ngamia wake wote. Yule mtu akamstaajabu, lakini akanyamaza, apate kujua, kama Bwana amemtimizia vema safari yake, au kama sivyo. Ngamia walipokwisha kunywa wote, yule mtu akatoa pete la dhahabu lenye uzito kama wa shilingi na vikuku viwili vya dhahabu vyenye uzito wa sekeli kumi, ndio robo ya ratli, akamtia mikononi pake, akamwuliza: Wewe binti nani? Tena niambie, kama nyumbani mwa baba yako mna mahali pa kulala sisi. Akamwambia: Mimi ni binti Betueli, mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori. Tena akamwambia: Majani ya kulisha ngamia kwetu ni mengi, hata mahali pa kulala usiku pako. Ndipo, yule mtu alipoinama na kumwangukia Bwana, akasema: Atukuzwe Bwana, Mungu wa bwana wangu Aburahamu, kwa kuwa hakuzikomesha huruma zake na welekevu wake kwa Bwana wangu. Mimi nami Bwana ameniongoza njiani, akanifikisha nyumbani mwa ndugu zake. Lakini yule kijana alikuwa amekimbilia nyumbani mwa mama yake kuyasimulia maneno hayo yote. Naye huyo Rebeka alikuwa na kaka yake, jina lake Labani; huyu Labani akamkimbilia yule mtu huko nje kwenye kisima. Alipokuwa ameliona lile pete na vile vikuku mikononi pa dada, tena alipokuwa ameyasikia hayo maneno ya dada yake Rebeka kwamba: Haya ndiyo, yule mtu aliyoniambia, basi, hapo ndipo, alipomwendea yule mtu, akamkuta, akisimama kisimani na ngamia wake, akasema: Karibu, uliyebarikiwa na Bwana! Kwa nini unasimama nje? Mimi nimekutengenezea nyumba, hata mahali pa ngamia. Yule mtu alipoingia nyumbani, huyu akawafungua ngamia mizigo yao, akawapa mabua ya kulalia na majani ya kulisha, naye mwenyewe akampa maji ya kuiosha miguu yake nayo miguu ya watu waliokuwa naye. Alipoandaliwa vyakula yule akasema: Sitakula, mpaka niyaseme maneno yangu. Akamwambia: Yaseme! Akasema: Mimi ni mtumishi wake Aburahamu. Bwana amembariki sana bwana wangu, akawa mkubwa, akampa mbuzi na kondoo na ng'ombe na fedha na dhahabu na watumwa wa kiume na wa kike na ngamia na punda. Naye Sara, mkewe bwana wangu, akamzalia bwana wangu mwana wa kiume alipokwisha kuwa mzee; yeye ndiye, aliyempa yote, aliyo nayo. Kisha bwana wangu akaniapisha kwamba: Usimposee mwanangu mwanamke miongoni mwao wana wa kike wa Wakanaani, ambao ninakaa katika nchi yao! Ila uende nyumbani mwa baba yangu kwenye ndugu zangu kumposea mwanangu mkewe! Nilipomwambia bwana wangu: Labda yule mwanamke hatanifuata, ndipo, aliponiambia: Bwana, ambaye ninafanya mwenendo machoni pake, atatuma malaika wake kwenda na wewe, akupe, safari yako ifanikiwe, umposee mwanangu mke kwao ndugu zangu waliomo nyumbani mwa baba yangu. Hapo utakapofika kwa ndugu zangu utakuwa uemfunguliwa, nacho kiapo, ninachokutakia, kitakuwa kimetanguka; usipompata kwao, utakuwa umefunguliwa kweli, nacho kiapo, ninachokutakia, kitakuwa kimetanguka kweli. Nilipofika leo hapo kisimani nikaomba kwamba: Bwana, Mungu wa bwana wangu Aburahamu, afadhali nipe, hii safari yangu, niliyokuja huku, ifanikiwe! Tazama ninasimama hapa penye kisima cha maji! Itakuwa, kijana wa kike atoke kuchota maji, nami nitakapomwambia: Nipe maji kidogo ya mtungini mwako, ninywe! naye akiniambia: Haya! Unywe wewe mwenyewe! nao ngamia wako nitawachotea, basi, awe yeye mwanamke, Bwana aliyemchagulia mwana wa bwana wangu! Mimi nilipokuwa sijaisha bado kuyasema moyoni mwangu, mara nikamwona Rebeka, akitokea mwenye mtungi wake begani pake, akashuka kisimani kuchota. Ndipo, nilipomwambia: Nipe maji, ninywe! Naye akaushusha upesi mtungi wake toka begani, akasema: Haya! Unywe! Nao ngamia wako nitawapa, wanywe. Nilipokwisha kunywa, akawanywesha ngamia nao. Kisha nikamwuliza kwamba: Wewe binti nani? Akasema: Mimi binti Betueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia Nahori. Ndipo, nilipotia pete puani mwake na vikuku mikononi pake. Nikainama na kumwangukia Bwana, nikamtukuza Bwana, Mungu wa bwana wangu Aburahamu, kwa kuwa ameniongoza njiani kweli, nipate kumposea mwana wa bwana wangu binti ndugu yake. Sasa ninyi kama mkimpatia bwana wangu huruma na welekevu, niambieni! Kama sivyo, niambieni vile vile, nipate kugeuka na kujiendea kuumeni au kushotoni! Ndipo, Labani na Betueli walipojibu kwamba: Neno hili lmetoka kwake Bwana, sisi hatuwezi kukuambia neno baya wala jema. Tazama! Rebeka yuko mbele yako; mchukue kwenda naye, awe mkewe mwana wa bwana wako, kama Bwana alivyosema. Mtumishi wake Aburahamu alipoyasikia maneno yao akamwangukia Bwana hapo chini. Kisha huyo mtumishi akatoa vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu na nguo, akampa Rebeka, naye umbu lake na mama yake akawapa matunzo. Wakala, wakanywa yeye nao wale watu waliokuwa naye, kisha wakalala. Asubuhi walipoamka, akawaambia: Nipeni ruhusa kwenda kwa bwana wangu! Lakini kaka yake na mama yake wakasema: Acha kwanza, huyu kijana akae kwetu siku kidogo kama kumi! Halafu atakwenda, Naye akamwambia: Msinikawilishe! Kwani Bwana amenipa, safari yangu ifanikiwe, nipeni ruhusa, niende kwa bwana wangu! Ndipo, waliposema: Na tumwite huyu kijana, tumwulize, tuone, atakayoyasema! Wakamwita Rebeka, wakamwuliza: Unataka kwenda na mtu huyu! Akasema: Nitakwenda. Ndipo, walipompa ndugu yao Rebeka ruhusa kwenda pamoja na yaya wake na mtumishi wa Aburahamu na watu wake. Wakambariki Rebeka, wakamwambia: Ndugu yetu, na uwe mama ya maelfu na maelfu! Nao wa uzao wako na wayakalie malango ya adui zao! Kisha Rebeka akaondoka na watumishi wake wa kike, wakipanda ngamia, wakamfuata yule mtu. Hivyo ndivyo, huyo mtumishi alivyomchukua Rebeka kwenda naye. Isaka alikuwa ametoka penye kisima cha Mwenye Uzima Anionaye, maana alikaa katika nchi ya kusini. Naye alikuwa ametoka kwenda shambani kuomba, jua lilipotaka kuchwa. Alipoyainua macho yake, mara akaona ngamia, wanaokuja. Rebeka naye akayainua macho yake; alipomwona Isaka akashuka upesi katika ngamia, akamwuliza yule mtumishi: Huyu mtu anayetujia hapa shambani ni nani? Yule mtumishi aliposema: Huyu ni bwana wangu, akachukua ukaya, akajifunika ushungi. Yule mtumishi akamsimulia Isaka mambo yote, aliyoyafanya. Ndipo, Isaka alipomwingiza Rebeka hemani mwa mama yake Sara, akamwoa, akawa mkewe, naye akampenda. Ndivyo Isaka alivyotulizwa moyo kwa ajili ya kufa kwa mama yake. Aburahamu akaoa tena, jina lake mkewe ni Ketura. Huyu akamzalia Zimurani na Yokisani na Medani na Midiani na Isibaki na Sua. Naye Yokisani akamzaa Saba na Dedani; nao wana wa Dedani walikuwa Waasuri na Waletusi na Walumu. Nao wana wa Midiani walikuwa Efa na Eferi na Henoki na Abida na Eldaa; hawa wote walikuwa wana wa Ketura. Kisha Aburahamu akampa Isaka yote pia, aliyokuwa aliyo. Lakini wana wa masuria, Aburhamu aliokuwa nao, Aburahamu akawapa matunzo, kisha akawatuma angaliko mzima kuondoka kwa mwanawe Isaka, waende upande wa maawioni kwa jua kukaa katika nchi ya huko maawioni kwa jua. Siku zote za miaka ya kuwapo kwake Aburahamu, aliyokuwapo, ni miaka 175. Kisha Aburahamu akazimia, akafa kwa kuwa mkongwe sana, naye alikuwa mzee aliyeshiba siku zake; ndipo, alipochukuliwa kwenda kwao walio wa ukoo wake. Wanawe Isaka na Isimaeli wakamzika mle pangoni mwa Makipela katika shamba la Yule Mhiti Efuroni, mwana wa Sohari, linaloelekea Mamure. Ndilo lile shamba, Aburahamu alilolinunua kwa wana wa Hiti; ndiko, Aburahamu alikozikwa na mkewe Sara. Aburahamu alipokwisha kufa, Mungu akambariki mwanawe Isaka. Naye Isaka akakaa kwenye kisima cha Mwenye Uzima Anionaye. Hivi ndiyo vizazi vya Isimaeli, mwana wa Aburahamu, ambaye Hagari wa Misri aliyekuwa kijakazi wake Sara alimzalia Aburahamu. Nayo haya ndiyo majina ya wana wa Isimaeli waliyoitwa hivyo, walivyofuatana kuzaliwa: Mwana wa kwanza wa Isimaeli ni Nebayoti, tena Kedari na Adibeli na Mibusamu, na Misima na Duma na Masa; Hadadi na Tema, Yeturi, Nafisi na Kedima. Hawa ndio wana wa Isimaeli, nayo haya ndiyo majina yao, waliyoitwa katika vijiji vyao na katika makambi ya mahema yao; nao walikuwa wakuu 12 wa makabila yao. Nayo hii ndiyo miaka ya kuwapo kwake Isimaeli, miaka 137; kisha akazimia, akafa, akachukuliwa kwenda kwao walio wa ukoo wake. Nao wale walikaa toka Hawila mpaka Suri unaoelekea Misri hata kufika Asuri; hivyo alikuwa ametua mbele yao ndugu zake wote. Hivi ndivyo vizazi vya Isaka, mwana wa Aburahamu: Aburahamu alimzaa Isaka. Isaka alikuwa mwenye miaka 40 alipomchukua Rebeka kuwa mkewe, naye alikuwa binti Betueli, Mshami na Mesopotamia, dada yake Mshami Labani. Isaka akamwombea mkewe kwake Bwana, kwani alikuwa mgumba; naye Bwana akayaitikia maombo yake, ndipo, mkewe Rebeka alipopata mimba, Watoto walipogongana tumboni mwake, akasema: Kama ndivyo, nimevipatia nini? Akaenda kumwuliza Bwana. Bwana akamwambia: Mataifa mawili yamo tumboni mwako, kabila mbili za watu zinatengana tumboni mwako zikitaka kutoka, kabila moja itatenda nguvu kuishinda ile nyingine, naye mkubwa atamtumikia nduguye. Siku zake za kuzaa zilipotimia, ikaonekana, ya kuwa wana wa pacha wamo tumboni mwake. Wa kwanza alipotoka alikuwa mwekundu, mwenye manyoya mwilini mote kama vazi la ngozi, wakamwita jina lake Esau. Ndugu yake alipotoka baadaye, mkono wake ulikuwa unakishika kisigino cha Esau, wakamwita jina lake Yakobo. Naye Isaka alikuwa mwenye miaka 60, mkewe alipowazaa. Hawa watoto walipokua, Esau akawa wa porini na fundi wa kuwinda, lakini Yakobo akawa mtulivu, akapenda kukaa hemani. Kwa hiyo Isaka akampenda Esau, kwa kuwa alimpatia nyama za kula za porini, lakini Rebeka alikuwa anampenda Yakobo. Siku moja Yakobo alipopika kunde, Esau akarudi toka porini, naye alikuwa amechoka sana. Ndipo, Esau alipomwambia Yakobo: Nipe, nile upesi hicho chekunduchekundu! Kwani nimechoka sana. Kwa sababu hii wakaliita jina lake Edomu (Mwekundu). Lakini Yakobo akasema: Niuzie leo hivi ukubwa wako! Naye Esau akasema: Tazama, mimi ninakwenda kufa! Hapo ukubwa utanifaa nini? Yakobo akasema: Uniapie leo hivi! Basi, akamwapia; hivyo ndivyo, alivyomwuzia Yakobo ukubwa wake. Kisha Yakobo akampa mkate na hizo kunde, alizozipika; naye akala, akanywa, kisha akainuka, akaenda zake. Hivyo ndivyo, Esau alivyoubeza ukubwa. Njaa ikaingia katika nchi hiyo kuliko ile njaa ya kwanza iliyokuwako siku za Aburahamu; ndipo, Isaka alipokwenda Gerari kwa Abimeleki, mfalme wa Wafilisti. Ndiko, Bwana alikomtokea na kumwambia: Usitelemke kwenda Misri! Kaa katika nchi, nitakayokuambia! Kaa ugenini katika nchi hii, mimi nitakuwa pamoja na wewe, nikubariki. Kwani wewe nao wa uzao wako nitawapa nchi hizi zote, nikitimize kiapo, nilichomwapia baba yako Aburahamu. Nitawafanya wao wa uzao wako kuwa wengi kama nyota za mbinguni, nazo nchi hizi zote nitawapa wao wa uzao wako, namo katika uazo wako ndimo, mataifa yote ya nchini yatakamobarikiwa, kwa kuwa Aburahamu aliisikia sauti yangu, akayaangalia maneno yangu yapasayo kuangaliwa: maagizo yangu na maongozi yangu na maonyo yangu. Isaka alipokaa Gerari, nao waume wa mahalai hapo walipomwuliza habari ya mkewe, akasema: Huyu ni dada yangu, kwani aliogopa kusema: Ni mke wangu, kwa kwamba: Waume wa mahali hapa wasije kuniua kwa ajili ya Rebeka, kwani ni mzuri wa kumtazama. Alipokwisha kukaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akaona, Isaka alivyomchekesha mkewe. Ndipo, Abimeleki alipomwita Isaka, akasema: Kumbe huyo ni mkeo! Umewezaje kusema: Huyu ni dada yangu? Isaka akamwambia: Ni kwa kuwa nilisema: Nisiuawe kwa ajili yake! Abimeleki akasema: Kwa nini umetufanyizia hivyo? Hili lingekuwa jambo kubwa, mtu wa kwetu akilala na mkeo, nawe ungalitukosesha sana. Kwa hiyo Abimeleki akawatangazia watu wake wote kwamba: Atakayemgusa mtu huyu au mkewe hana budi kuuawa. Isaka alipopanda mbegu katika nchi hiyo, akavuna mia mwaka huo, maana Bwana alimbariki. Akawa mtu mkuu, akaendelea vivyo hivyo kuwa mkuu, mpaka akiwa mkuu kabisa. Akawa na makundi ya mbuzi na kondoo, nayo makundi ya ng'ombe, nao watumwa wengi, kwa hiyo Wafilisti wakamwonea wivu; navyo visima vyote, watumwa wa baba yake walivyovichimbua siku za baba yake Aburahamu, Wafisiti walikuwa wameviziba na kuvijaza mchanga. Naye Abimeleki akamwambia Isaka: Toka kwetu! Kwani umepata nguvu za kutushinda sisi kabisa. Basi, Isaka akatoka huko, akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Ndipo, alipovirudia na kuvichimbua tena vile visima vya maji, walivyovichimbua siku zile za baba yake Aburahamu, Wafilisti walivyoviziba, Aburahamu alipokwisha kufa, akaviita majina yaleyale, baba yake aliyoviita. Namo mle bondeni, watumwa wa Isaka walipochimba maji, wakapata kisima chenye maji yarukayo. Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana nao wachungaji wa Isaka kwamba: Maji ni yetu! Ndipo, alipokiita hicho kisima jina lake Eseki (Ukorofi), kwa kuwa walimkorofisha huko. Walipochimbua kisima kingine, wakagombana nao hata kwa ajili yake hicho, akakiita jina lake Sitina (Upingani). Kisha akayavunja mahema yake huko, akachimbua kisima kingine; kwa kuwa hawakugombana naye kwa ajili yake hicho, akakiita jina lake Rehoboti (Papana) akisema: Sasa Bwama ametupanulia, tupate kuenea katika nchi hii. Kisha akatoka huko kwenda kupanda Beri-Seba. Huko Bwana akamtokea usiku uleule, akamwambia: Mimi ni Mungu wa baba yako Aburahamu; usiogope! Kwani mimi niko pamoja na wewe, nikubariki na kuwafanya wao wa uzao wako kuwa wengi kwa ajili ya mtumishi wangu Aburahamu. Ndipo, Isaka alipojenga huko pa kutambikia, akalitambikia Jina la Bwana, akalipiga hema lake huko, nao watumwa wake Isaka wakachimbua huko kisima. Huko Abimeleki na rafiki zake Ahuzati na Pikoli, mkuu wa vikosi, wakamwendea na kutoka Gerari. Isaka akawauliza: Kwa nini mmekuja kwangu ninyi mnaonichukia, mkanifukuza kwenu? Wakasema: Tumeona kwa macho yetu, ya kuwa Bwana yuko pamoja na wewe, kwa hiyo tukasema: Na tufanye maagano na wewe na kuapiana sisi na wewe! Usitufanyie mabaya, kama sisi tusivyokugusa, kama sisi tulivyokufanyia mema tu, tukakuacha, uende zako na kutengemana. Nawe sasa umebarikiwa hivyo na Bwana. Ndipo, alipowafanyia karamu, wakala, wakanywa. Kesho yake wakaamka na mapema, wakaapiana kila mmoja na mwenziwe, kisha Isaka akawasindikiza, wakitoka kwake kwenda zao na kutengemana. Ikawa siku hiyo, wakaja watumwa wake Isaka kumpasha habari za kile kisima, walichokichimbua, wakamwambia: Tumeona maji. Naye akakiita jina lake Siba (Kiapo); kwa sababu hii mji huo unaitwa jina lake Beri-Seba (Kisima cha Kiapo) mpaka siku hii ya leo. Esau alipokuwa mwenye miaka 40 akamwoa Yuditi, binti Mhiti Beri; kisha naye Basimati, binti Mhiti Eloni. Wote wawili wakamtia Isaka naye Rebeka uchungu mwingi rohoni. Ikawa, Isaka alipokuwa mkongwe, macho yake yakatenda kiza, yasione; ndipo, alipomwita mwanawe mkubwa Esau, akamwambia: Mwanangu! Naye akamwitikia: Mimi hapa! Akasema: Tazama, nimekuwa mkongwe, siijui siku ya kufa kwangu. Sasa yachukue mata yako, ndio podo lako na upindi wako, uende porini kuniwindia nyama! Kisha unitengenezee kilaji cha urembo, kama ninavyokipenda, uniletee, nile, roho yangu ipate kukubariki, nikingali bado sijafa. Lakini Rebeka alikuwa ameyasikia, Isaka aliyomwambia mwanawe Esau. Esau alipokwisha kwenda porini kuwinda nyama ya kumpelekea baba, Rebeka akamwambia mwanawe Yakobo kwamba: Tazama, nimesikia, baba yako akimwambia kaka yako Esau kwamba: Niletee nyama ya porini, unitengenezee kilaji cha urembo, nile, nipate kukubariki usoni pa Bwana kabla ya kufa kwangu! Sasa mwanangu, isikie sauti yangu, uyafanye nitakayokuagiza! Nenda makundini kunichukulia huko wana wawili wa mbuzi walio wazuri, nimtengenezee baba yako nyama zao kuwa kilaji cha urembo, kama anavyokipenda. Kisha utampelekea baba yako, ale, apate kukubariki kabla ya kufa kwake. Lakini Yakobo akamwambia mama yake Rebeka: Tazama, kaka yangu Esau ni mwenye manyoya, lakini mimi sinayo. Labda baba atanipapasa; ndipo, nitakapokuwa kama mdanganyifu machoni pake; hivyo nitajipatia maapizo, sio mbaraka. Naye mama yake akamwambia: Maapizo yako na yanijie mimi, mwanangu! Isikie tu sauti yangu, uende kunichukulia wana wa mbuzi! Ndipo, alipokwenda, akawachukua, akamplekea mama yake, naye mama yake akawatengeneza kuwa kilaji cha urembo, kama baba yake alivyokipenda. Kisha Rebeka akazichukua nguo za mwanawe mkubwa Esau zilizo nzuri mno, alizokuwa nazo nyumbani mwake, akamvika mwanawe mdogo Yakobo. Nazo ngozi za wale wana wa mbuzi akamvika mikononi namo shingoni mlimokuwa hamna manyoya. Kisha akampa mwanawe Yakobo mkononi mwake hicho kilaji cha urembo pamoja na mkate, alioutengeneza nao. Alipoingia mwa baba yake akasema: Baba! Naye akasema: Mimi hapa! Wewe ndiwe nani, mwanangu? Yakobo akamwambia baba yake: Mimi ni Esau, mwanao wa kwanza; nimefanya, kama ulivyoniagiza. Inuka, ukae, ule nyama zangu, nilizokuwindia, roho yako ipate kunibariki! Isaka akamwuliza mwanawe: Mwanangu, umepataje nyama upesi hivyo? Akasema: Bwana Mungu wako amemtuma, anijie njiani. Kisha Isaka akamwambia Yakobo: Nikaribie, mwanangu, nikupapase, nione, kama wewe ndiwe mwanangu Esau, au kama siwe! Yakobo akamkaribia baba yake Isaka, akampapasa, akasema: Sauti ni sauti yake Yakobo, lakini mikono ni mikono yake Esau. Hakumtambua, kwa kuwa mikono yake ilikuwa kama mikono ya kaka yake Esau yenye manyoya; ndipo, alipombariki. Alipomwuliza tena: Wewe ndie kweli mwanangu Esau? akasema: Ndio, ni mimi. Ndipo, alipomwambia: Niletee karibu, nile nyama, ulizoniwindia, mwanangu, roho yangu ipate kukubariki! Akazileta karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa. Kisha baba yake Isaka akamwambia: Nikaribie, uninonee, mwanangu! Alipomkaribia na kumnonea, akausikia mnuko wa mavazi yake, akambariki akisema: Tazama! Mnuko wa mwnangu ni kama mnuko wa shamba, Bwana alilolibariki. Mungu akugawie umande wa mbinguni na manono ya nchi, ngano zako ziwe nyingi, hata mvinyo vilevile! Makabila mazima na yakutumikie, koo za watu zikuangukie! Na uwe mkuu wa ndugu zako, wana wa mama yako wakuangukie! Atakayekuapiza na naapizwe! Atakayekubariki na abarikiwe naye! Ikawa, Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, naye Yakobo alipokwisha kutoka usoni pa baba yake Isaka, ndipo, kaka yake Esau aliporudi kwa kuwinda. Naye akatengeneza kilaji cha urembo, akampelekea baba yake, akamwambia baba yake: Baba, inuka, ule nyama, mwanao alizokuwinda, roho yako ipate kunibariki! Ndipo, baba yake Isaka alipomwuliza: Wewe ndiwe nani? Akajibu: Mimi ni mwanao wa kwanza Esau. Ndipo, Isaka aliposhangaa mshangao mkubwa mno, akasema: Sasa ni nani yule mwinda nyama aliyeniletea nyama, nikala, ulipokuwa hujaja bado, nikambariki? Naye atakuwa amebarikiwa. Esau alipoyasikia haya maneno ya baba yake, akalia kilio kikubwa chenye uchungu mwingi sana, akamwambia baba yake: Baba, nibariki mimi nami! Lakini akajibu: Ndugu yako mekuja kwa udanganyifu, akaipaat mbaraka yako. Akasema: Kumbe haitwi jina lake Yakobo (Mdanganyi)? Naye amenidanganya sasa mara mbili: Kwanza ameuchukua ukubwa wangu, sasa ameichukua mbaraka yangu nayo. Kisha akauliza: Hukuniwekea mbaraka nami? Isaka akajibu na kumwambia Esau: Tazama! Nimemweka kuwa mkubwa wako, nao ndugu zake wote nimempa, wamtumikie, hata ngano na mvinyo nimemfurikishia. Nawe wewe, mwanangu, nikufanyie nini? Ndipo, Esau alipomwuliza baba yake: Baba, unayo mbaraka moja tu? Baba, nibariki mimi nami! Kisha Esau akaipaza sauti yake, akalia. Ndipo, baba yake Isaka alipomwitikia na kumwambia: Tazama! Hapo, utakapokaa, manono ya nchi yatakuwa mbali, nao umande wa mbinguni juu. Utajilisha mapato ya upanga wako, utamtumikia ndugu yako; lakini itakuwa, ukijikaza utalivunja kongwa, litoke shingoni pako! Esau akamchukua Yakobo kwa ajili ya hiyo mbaraka, baba yake aliyombariki; kwa hiyo Esau akasema moyoni mwake: Siku za kumwombolezea baba ziko karibu; zitakapopita, nitamwua ndugu yangu Yakobo. Rebeka alipopata habari ya lile shauri la mwananwe mkubwa Esau, akatuma kumwita mwanawe mdogo Yakobo, akamwambia: Tazama! Kaka yako Esau anajituliza moyo kwa kwamba, akuue. Sasa mwnanangu, isikie sauti yangu! Inuka, ukimbilie Harani kwa kaka yangu Labani! Na ukae kwake siku kidogo, mpaka machafuko ya kaka yako yatulie. Hapo, haya makali ya kaka yako yatakapotulia, aache kukuwazia mabaya kwa kuyasahau uliyomfanyizia, ndipo, nitakapotuma kukuchukua huko. Kwa nini mwataka, nifiwe nanyi wawili siku moja? Kisha Rebeka akamwambia Isaka: Ninachukizwa sana na kuwapo kwangu kwa ajili ya hao wanawake wa Kihiti. Kama Yakobo naye ataoa mwanamke miongoni mwao vijana wa kike wa Kihiti walio hivyo, kama hawa walivyo miongoni mwa vijana wa nchi hii, mimi nimeletewa nini huku? Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza kwamba: Usioe mwanamke katika vijana wa kike wa Kanaani! Inuka, uende Mesopotamia nyumbani mwa Betueli, babake mama yako, umchukue mkeo huko katika wana wa kike wa Labani, umbu lake mama yako. Naye Mwenyezi Mungu akubariki, akupe kuzaa wana wengi sana, upate kuwa mkutano wa makabila ya watu! Akupe nayo mbaraka ya Aburahamu, wewe nao wa uzao wako wajao, upate kuichukua nchi hii ya ugeni wako, Mungu aliyompa Aburahamu. Ndivyo, Isaka alivyomtuma Yakobo kwenda Mesopotamia kwa Mshami Labani, mwana wa Betueli, kaka yake Rebeka aliyekuwa mama yao Yakobo na Esau. Esau akaona, ya kuwa Isaka amembariki Yakobo na kumtuma kwenda Mesopotamia, achukue mke huko, tena ya kuwa hapo alipombariki amemwagiza kwamba: Usijichukulie mke katika vijana wa kike wa Kanaani! Tena akaona, ya kuwa Yakobo amemsikia baba yake na mama yake alipokwenda Mesopotamia. Tena Esau akaona, ya kama vijana wa kike wa Kanaani walikuwa wabaya machoni pa baba yake, Isaka. Ndipo, Esau alipokwenda kwa Isimaeli, akamchukua Mahalati, binti Isimaeli, mwana wa Aburahamu, umbu lake Nebayoti, kuwa mkewe pamoja na wakeze, aliokuwa nao. Yakobo akaondoka Beri-Seba, akaenda Harani. Njiani alipofika mahali palipomfaa akalala hapo usiku, kwani jua lilikuwa limekuchwa. Akachukua jiwe la hapo, akaliweka chini ya kichwa chake, akalala mahali pale. Akaota, akaona ngazi, ilikuwa imesimikwa nchini, lakini ncha yake iligusa mbinguni; alipotazama akona, malaika wa Mungu wakipanda, tena wakishuka hapo. Naye Bwana akamwona, akisimama juu, akasema: Mimi ni Bwana, Mungu wa baba yako Aburahamu na Mungu wa Isaka. Nchi hii, unayoilalia, nitakupa wewe nao wa uzao wako. Nao wa uzao wako watakuwa wengi kama mavumbi ya nchi hii, nawe utaenea upande wa baharini na upande wa maawioni kwa jua na upande wa kaskazini na upande wa kusini; namo mwako na katika uzao wako ndimo, koo zote za nchini zitakamobarikiwa. Tazama! Niko pamoja na wewe, nikulinde po pote, utakapokwenda; nitakurudisha katika nchi hii, kwani sitakuacha, mpaka niyafanyize, niliyokuambia wewe. Yakobo alipoamka katika usingizi akasema: Kweli Bwana yuko mahali hapa, nami nilikuwa sikuyajua. Kwa hiyo akaogopa, akasema: Kumbe mahali hapa panaogopesha, hapa sipo pengine, ndipo Nyumba ya Mungu ilipo, ndipo lango la mbingu lilipo. Asubuhi na mapema Yakobo akaamka, akalichukua lile jiwe, aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimika kuwa kielekezo, akalimiminia mafuta juu yake, akapaita mahali pale jina lake Beteli (Nyumba ya Mungu), lakini kwanza ule mji uliitwa Luzi. Kisha Yakobo akaapa kiapo kwamba: Mungu akiwa pamoja na mimi na kunilinda katika safari hii, ninayokwenda, akinipa vilaji vya kula na nguo za kuvaa, nipate kurudi na kutengemana nyumbani mwa baba yangu, Bwana atakuwa Mungu wangu, hata jiwe hili, nililolisimika kuwa kielekezo, litakuwa Nyumba ya Mungu, nayo yote, utakayonipa, nitakutolea fungu la kumi. Kisha Yakobo akashika njia kwenda katika nchi yao wana wa upande wa maawioni kwa jua. Huko akaona kisima njiani, tena akaona makundi matatu ya mbuzi na kondoo waliopumzika hapo, kwani humo kisimani ndimo, walimonyweshea makundi yao, nalo jiwe lililowekwa juu mdomoni pa kisima lilikuwa kubwa. Huko ndiko, makundi yote yalikokusanyikia, kisha wakaliondoa hilo jiwe mdomoni pa kisima na kulifingirisha; tena walipokwisha kuyanywesha makundi yao, wakalirudisha mahali pake mdomoni pa kisima. Naye Yakobo akawauliza: Ndugu, mnatoka wapi? Wakasema: Tumetoka Harani. Akawauliza: Mwamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakajibu: Twamjua. Akawauliza tena: Hajambo? Wakajibu: Hajambo, tena tazama! Mwanawe wa kike, Raheli, anakuja na kundi lake. Akasema: Tazameni, jua liko juu bado, saa za kukusanyikia makundi hazijatimia bado; wanywesheni mbuzi na kondoo, kisha walisheni! Wakajibu: Hatuwezi, mpaka makundi yote yakusanyike, wote waliondoe hili jiwe na kulifingirisha, tupate kuwanywesha mbuzi na kondoo. Angali akisema nao, Raheli akafika na kundi la baba yake, kwani alikua analichunga. Yakobo alipomwona Raheli, binti Labani aliyekuwa umbu la mama yake, nalo kundi la Labani aliyekuwa umbu la mama yake, Yakobo akafika karibu, akalifingirisha lile jiwe, liondoke mdomoni pa kisima, akawanywesha mbuzi na kondoo wa Labani aliyekuwa umbu la mama yake. Kisha Yakobo akamnonea Raheli, akaipaza sauti yake na kulia. Yakobo akamsimulia Raheli, ya kuwa yeye ni ndugu ya baba yake kwa kuwa mwana wa Rebeka; ndipo, alipopiga mbio kwenda kumpasha baba yake habari. Ikawa, Labani alipozisikia habari za Yakobo, mwana wa umbu lake, akamkimbilia, akamkumbatia na kumnonea, kisha akampeleka nyumbani mwake. Naye akamsimulia Labani hayo mambo yote ya kwao. Ndipo, Labani alipomwambia: Kweli wewe na mimi tu mfupa mmoja na nyama za mwili mmoja. Akakaa kwake siku kama za mwezi mmoja. Kisha Labani akamwambia Yakobo: Ijapo u ndugu yangu, kwa hiyo utanitumikia bure? Niambie mshahara wako, unaoutaka! Naye Labani alikuwa na wana wa kike wawili, mkubwa jina lake ni Lea, mdogo jina lake ni Raheli. Macho yake Lea yalikuwa yemepumbaapumbaa, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo lake na wa uso wake. Kwa hiyo Yakobo akampenda Raheli, akasema: Nitakutumikia miaka saba, unipe mwanao mdogo Raheli. Labani akasema: Inafaa zaidi, nikupe wewe kuliko mtu mwingine; basi, kaa kwangu! Yakobo akamtumikia miaka saba, ampate Raheli, nayo ilikuwa machoni pake kama siku chache tu kwa kumpenda sana. Kisha Yakobo akamwambia Labani: Nipe mke wangu! Kwani siku zangu zimetimia, nipate kuingia kwake. Ndipo, Labani alipowakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya karamu. Ilipokuwa jioni, akamchukua mwanawe Lea, akamwingiza kwake, naye akaingia kwake. Naye Labani akampa kijakazi wake Zilpa, amtumikie mwanawe Lea. Ilipokuwa asubuhi, Yakobo akaona, ya kama ndiye Lea; ndipo, alipomwuliza Labani: Mbona umenifanyizia hivyo? Sikukutumikia kumpata Raheli? Kwa nini umenidanganya? Labani akasema: Huku kwetu haiwezekani kumwoza mdogo, mkubwa wake akiwa hajaolewa. Maliza naye juma hili la ndoa, halafu tutakupa naye yule, ukinitumika tena miaka saba mingine. Yakobo akafanya hivyo, akalimaliza juma hilo la ndoa, kisha akampa naye mwanawe Raheli kuwa mkewe. Naye mwanawe Raheli Labani akampa kijakazi wake Biliha, amtumikie. Hivyo akapata kuingia hata kwake Raheli, akampenda kuliko Lea; kwa kumpata naye akamtumikia tena miaka saba mingine. Bwana alipoona, ya kuwa Lea amechukiwa naye, akalifungua tumbo lake, lakini Raheli alikuwa mgumba. Ndipo, Lea alipopata mimba, akazaa mtoto mume, akamwita jina lake Rubeni (Tazameni Mtoto), kwani alisema: Bwana ameutazama ukiwa wangu; kwani sasa mume wangu atanipenda. Akapata mimba tena, akazaa mtoto mume, akasema: Kwa kuwa Bwana amesikia, ya kama nimechukiwa, amenipa huyu mtoto naye, kwa hiyo akamwita jina lake Simeoni (Kusikiwa). Akapata mimba tena, akazaa mtoto mume, akasema: Sasa mara hii mume wangu ataandamanishwa na mimi, kwa kuwa nimemzalia watoto waume watatu, kwa hiyo akamwita jina lake Lawi (Mwandamano). Akapata mimba tena, akazaa mtoto mume, akasema: Mara hii nitamshukuru Bwana, kwa hiyo akamwita jina lake Yuda (Shukrani). Kisha akakoma kuzaa. Raheli alipoona, ya kuwa hamzalii Yakobo wana, ndipo, alipomwonea dada yake wivu, akamwambia Yakobo: Unipatie wana! Nisipowapata nitakufa. Ndipo, makali ya Yakobo yalipomwakia Raheli, akamwambia: Je? Mimi ni kama Mungu aliyekunyima mazao ya tumbo? Akajibu: Tazama! Yuko kijakazi wangu Biliha, ingia kwake, azae magotini pangu, mimi nami nipate mlango kwake yeye. Akampa kijakazi wake Biliha kuwa mkewe, naye Yakobo akaingia kwake. Hivyo Biliha akapata mimba, akamzalia Yakobo mtoto mume. Ndipo, Raheli aliposema: Mungu amenihukumia, akaisikia nayo sauti yangu, akanipa mtoto mume, kwa sababu hii akamwita jina lake Dani (Mhukumu). Kisha Biliha, kijakazi wake Raheli, akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mtoto mume wa pili. Raheli akasema: Nimepiga vita vya Mungu vya kupigana na dada yangu, nami nikashinda. Kwa hiyo akamwita jina lake Nafutali (Vita vyangu). Lea alipoona, ya kuwa amekoma kuzaa, akamchukua kijakazi wake Zilpa, akampa Yakobo kuwa mkewe. Huyu Zilpa, kijakazi wake Lea, akamzalia Yakobo mtoto mume; ndipo, Lea aliposema: Nina bahati, akamwita jina lake Gadi (Bahati). Zilpa, kijakazi wake Lea, akamzalia Yakobo mtoto mume wa pili; ndipo, aliposema: Mimi ni mwenye shangwe, kwani wanawake watanishangilia. Kwa hiyo akamwita jina lake Aseri (Shangwe). Rubeni alipotembea siku za mavuno ya ngano, akaona tunguja shambani akampelekea mama yake. Naye Raheli akamwambia Lea: Unigawie na mimi tunguja za mwanao! Lakini huyu akajibu: Haitoshi, ukimchukua mume wangu? Unazitakia nini hizi tunguja za mwanangu? Raheli akajibu: Basi, na alale kwako usiku huu, nipate tu tunguja za mwanao! Jioni Yakobo aliporudi toka shambani, Lea akamwendea njiani, akamwambia: Ingia kwangu! Kwani nimekununua leo kwa kutoa tunguja za mwanangu. Alipolala naye usiku huo, Mungu akamsikia Lea, akapata mimba, akamzalia Yakobo mtoto mume wa tano. Ndipo, Lea aliposema: Mungu amenipa mshahara wangu, kwa kuwa nimempa mume wangu kijakazi wangu, kwa hiyo akamwita jina lake Isakari (Mtu wa Mshahara). Lea akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mtoto mume wa sita; ndipo, Lea aliposema: Mara hii Mungu amenipatia tunzo zuri. Sasa mume wangu atakaa kwangu, kwani nimemzalia watoto waume sita; kwa hiyo akamwita jina lake Zebuluni (Kao.) Baadaye akazaa mtoto mke, akamwita jina lake Dina. Ndipo, Mungu alipomkumbuka Raheli, Mungu akamsikia, akalifungua tumbo lake. Kwa hiyo naye akapata mimba, akazaa mtoto mume, akasema: Mungu ameniondolea yaliyonitia soni, akamwita jina lake Yosefu (Huongeza) akisema: Bwana aniongezee mwana mwingine! Raheli alipokwisha kumzaa Yosefu, Yakobo akamwambia Labani: Nipe ruhusa, niende kwetu katika nchi yangu! Nipe wake zangu na wanangu, ambao nilikutumikia, niwapate! Kisha niende zangu, kwani wewe unaujua utumishi wangu, niliokutumikia. Naye Labani akamwambia: Ninataka kuona upendeleo machoni pako, kwa kuwa nimeona, ya kama Bwana amenibariki kwa ajili yako. Akaendelea kusema: Ninakuomba, sema mshahara, unaotaka kwangu! Ndio, nitakaokupa. Akamwambia: Wewe unajua mwenyewe, jinsi nilivyokutumikia, tena jinsi makundi yako yalivyokua kwangu. Kwani kabla ya kuja kwangu yalikuwa madogo, lakini sasa yamesambaa kwa kuwa mengi, maana Bwana amekubariki pote, nilipokwenda. Sasa wao waliomo nyumbani mwangu niwafanyie kazi lini? Naye akamwuliza: Nikupe nini? Yakobo akamwambia: Usinipe cho chote! Nifanyie hili tu: acha, niwachunge tene mbuzi na kondoo wako na kuwaangalia! Tena nipite leo kwenye mbuzi na kondoo wako wote kuondoa kwao kondoo wote wenye mawaa na madoadoa nao wana weusi wote pia nao mbuzi wote wenye madoadoa na mawaa; basi, watakaozaliwa kuwa hivyo ndio mshahara wangu. Navyo ndiyo, nitakavyojulikana katika siku zijazo kuwa mwenye kweli: utakapokuja kuwatazama walio mshahara wangu, kila mbuzi asiye mwenye madoadoa na mawaa naye kila kondoo asiye mweusi atakuwa amekwibwa na mimi. Labani akamwitikia kwamba: Basi, na viwe hivyo, ulivyosema! Kisha Labani akaondoa siku hiyohiyo madume ya mbuzi wote waliokuwa wenye madoadoa na mawaa nao majike ya mbuzi wote waliokuwa wenye madoadoa na mawaa, wote pia waliokuwa wenye peupe, nao kondoo weusi wote, akawatia mikononi mwa wanawe, akawapeleka mwendo wa siku tatu, pawe hapo mahali pakubwa katikati yake yeye na Yakobo. Kisha Yakobo akapata kuwachunga mbuzi na kondoo wake Labani waliosalia. Kisha Yakobo akajitwalia matawi mabichi ya mikumbi na ya milozi na ya migude, akayabanduabandua, yapate mabaka meupe ya kutokeza sana huo weupe penye hayo matawi. Kisha akayasimika hayo matawi, aliyoyabandua hivyo, penye birika za kuwanyweshea maji mbuzi na kondoo kwamba: wao wakija kunywa maji, wayaone hayo, wanyegeshwe wakija kunywa. Nao mbuzi na kondoo waliponyegeshwa mbele ya hao matawi, ndipo, hao mbuzi na kondoo walipozaa wenye madoadoa na vipakupaku na mawaa. Hawa wana mbuzi Yakobo akawatenga, akawatanguliza mbele ya mbuzi na kondoo wengine, hao wote waliokuwa wake Labani wawatazame wale wenye madoadoa nao mbuzi na kondoo weusi; hivyo akajipatia makundi yake yeye, nayo haya hakuyachanganya nayo yake Labani. Kila mara mbuzi na kondoo wenye nguvu waliponyegeshwa, Yakobo akayaweka yale matawi machoni pao mbuzi na kondoo penye birika, wazidi kunyegeshwa wakiyaona hayo matawi. Lakini kwao wale mbuzi na kondoo waliokuwa wanyonge hakuyaweka; kwa sababu hii wale wanyonge wakawa wake Labani, lakini wale wenye nguvu wakawa wake Yakobo. Hivyo ndiyo, huyu mtu alivyopata mali nyingi sanasana, mbuzi na kondoo wake wakawa wengi, nao watumwa wa kiume na wa kike na ngamia na punda alikuwa nao. Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani kwamba: Yakobo ameyachukua yote yaliyokuwa ya baba yetu; katika hayo yaliyokuwa yake baba yetu ndimo, alimoyatoa hayo mapato yake yote. Ndipo, Yakobo alipoutazama uso wake Labani, akauona kuwa sio uleule, aliomwonyesha siku zote. Naye Bwana akamwabia Yakobo: Rudi katika nchi ya baba zako kwenye ndugu zako! Mimi nitakuwa pamona na wewe. Ndipo, Yakobo alipotuma kumwita Raheli naye Lea, waje porini kwake kwenye mbuzi na kondoo wake. Akawaambia: Mimi nimeuona uso wa baba yenu kuwa sio, alionionyesha jana na juzi, lakini Mungu wa baba yangu alikuwa pamoja na mimi. Nanyi mnajua, ya kuwa nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote. Lakini baba yenu amenidanganya na kuugeuza mshahara wangu mara kumi, lakini Mungu amemzuia, asiweze kunifanyizia kibaya. Aliposema: Wenye madoadoa watakuwa mshahara wako, mbuzi wote wakazaa wenye madoadoa; tena aliposema: Wenye vipakupaku watakuwa mshahara wako, mbuzi wote wakawa wenye vipakupaku. Ndivyo, Mungu alivyoyachukua makundi ya baba yenu, akanipa mimi. Ikawa siku zile, mbuzi waliponyegeshwa, nikayainua macho yangu, nikatazama katika ndoto, nikaona, madume waliowapanda majike walikuwa wenye vipakupaku na wenye madoadoa na wenye marakaraka. Naye malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto: Yakobo! Nikasema: Mimi hapa! Akasema: Yainue macho yako, utazame, madume wote wanaowapanda majike ni wenye vipakupaku na wenye madoadoa na wenye marakaraka. Kwani nimeyaona yote, Labani aliyokufanyia. Mimi ni Mungu wa Beteli, ulikolipaka mafuta lile jiwe, ulilolisimika, na kuniapia kiapo. Sasa inuka, utoke katika nchi hii, urudi katika nchi hiyo, uliyozaliwa! Ndipo, Raheli na Lea walipomjibu na kumwambia: Je? Sisi tuko na mafungu nyumbani mwa baba yetu, tutakayoyatwaa, yawe yetu sisi? Hatuwaziwi naye kuwa wageni, kwa kuwa ametuuza, akazila nazo zile fedha zetu? Kwani mali hizo zote, Mungu alizozichukua kwa baba yetu, ni zetu sisi na za wana wetu; sasa yote, Mungu aliyokuambia, yafanye! Ndipo, Yakobo alipoondoka, nao wanawe na wake akawapandisha juu ya ngamia, akayachukua nayo makundi yake yote na mapato yake yote, aliyoyapata, nao nyama wengine waliokuwa mali zake, alizozipata kule Mesopotamia, aende kwa baba yake Isaka katika nchi ya Kanaani. Lakini Labani alikuwa amekwenda kuwakata kondoo wake manyoya. Kwa hiyo Raheli akapata kuviiba vinyago vya nyumbani vya baba yake. Ndivyo, Yakobo alivyomdanganya Mshami Labani, kwa kuwa hakumpasha habari, ya kama anataka kujiendea upesi hivi. Akatoroka yeye pamoja nayo yote yaliyokuwa yake, akalivuka lile jito na kuuelekeza uso wake kwenda mlimani kwa Gileadi. Siku ya tatu Labani akapashwa habari, ya kuwa Yakobo ametoroka. Ndipo, alipowachukua ndugu zake, akapiga mbio za kumfuata safari ya siku saba, akampata mlimani kwa Gileadi. Lakini Mungu akamjia Mshami Labani katika ndoto usiku, akamwambia: Jiangalie, usiseme na Yakobo kwa ukali, ila kwa upole tu! Labani alimpofikia Yakobo karibu, Yakobo alikuwa amepiga hema lake mlimani, naye Labani na ndugu zake wakapanga mlimani kwa Gileadi. Labani akamwambia Yakobo: Umewezaje kuyafanya haya na kunidanganya, ukiwapeleka wanangu wa kike kama mateka wa upanga? Kwa nini umetoroka na kujifichaficha na kunidanganya, usiponipasha habari, nikapata kukusindikiza kwa furaha na kuimba na kupiga patu na mazeze? Wala hukunipatia kunoneana na wanangu wa kiume na wa kike. Kweli umefanya upumbavu. Ningependa, mkono wangu ungeweza kuwafanyizia mabaya, lakini Mungu wa baba yenu ameniambia usiku huu kwamba: Jiangalie, usiseme na Yakobo kwa ukali, ila kwa upole tu! Tena ulipokwenda safari yako kwa kuitunukia sana nyumba ya baba yako, kwa nini umekwiba miungu yangu? Yakobo akajibu na kumwambia Labani: Ni kwa kuwa nimeogopa na kusema moyoni, usininyang'anye wanao wa kike. Lakini utakayemwona, ya kuwa anayo miungu yako, na afe hapa mbele ya ndugu zetu! Jitafutie yaliyo yako kwangu, uyachukue! Naye Yakobo hakujua, ya kuwa Raheli ameiiba. Labani alipoingia hemani mwa Yakobo namo hemani mwa Lea namo hemani mwa wale vijakazi wawili hakuona kitu. Alipotoka hemani mwa Lea akaingia hemanai mwa Raheli. Lakini Raheli alikuwa amevificha vinyago vya nyumbani ndani ya matandiko ya ngamia, akayakalia. Naye Labani alipoyapapasapapasa yote yaliyomo hemani hakuona kitu. Naye Raheli akamwambia baba yake: Usikasirike, bwana wangu! Kwani siwezi kuinuka mbele yako, kwani mambo yetu ya kike yamenipata. Kwa hiyo hakuviona vile vinyago vya nyumbani, ijapo alivitafuta po pote. Ndipo, Yakobo alipokasirika sana, akaanza kumgombeza Labani akianza kusema naye na kumwambia: Nimepotoa nini? Au nimekosa nini, ukijikaza kunifuata hivyo? Umevipapasapapasa vyombo vyangu vyote pia, lakini umeona kitu gani kilicho cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya ndugu zangu walio na ndugu zako, watuamue sisi wawili. Sasa mimi nimekuwa miaka 20 kwako, majike wako wa kondoo na wa mbuzi hawakuharibu mimba, wala madume wako wa mbuzi na wa kondoo sikuwala. Walioraruliwa na nyama sikukupelekea, sikuwa na budi kuwalipa, ukawataka mikononi mwangu nao walioibiwa mchana, nao walioibiwa usiku. Mambo yangu yamekuwa hivyo: mchana joto la jua limenichoma, usiku nao baridi ikafukuza usingizi, usiingie machoni pangu. Hivyo ndivyo, nilivyokutumikia nyumbani mwako miaka hii 20, miaka kumi na minne, niwapate hawa wano wawili wa kike, tena miaka sita, niyapate haya makundi yako, nawe umeugeuza mshahara wangu mara kumi. Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Aburahamu, Isaka anayemcha naye, asingalikuwa upande wangu, ungalinifukuza sasa mikono mitupu. Lakini Mungu ameuona ukiwa wangu na usumbufu wa mikono yangu, kwa hiyo amekata shauri usiku huu. Labani akajibu na kumwambia Yakobo: Hawa wana wa kike ni wanangu, nao hawa wana ni wangu, nao hawa mbuzi na kondoo ni mbuzi na kondoo wangu, nayo yote, unayoyaona, ni yangu mimi. Basi, hawa wanangu wa kike nao hawa wana wao niwafanyie nini? Sasa njoo, tufanye agano mimi na wewe, lipate kutushuhudia mimi na wewe! Ndipo, Yakobo alipochukua jiwe, akalisimika kuwa kielekezo. Kisha yakobo akawaambia ndugu zake, waokote mawe; ndipo, walipokwenda kuchukua mawe, wakayapanga kuwa chungu, kisha wakaja juu yake hilo chungu. Labani akaliita Yegari-Sahaduta (Chungu la Ushahidi), naye Yakobo akaliita Galeedi (Chungu Shahidi). Labani akasema; Chungu hili leo ni shahidi wetu mimi na wewe, kwa hiyo likaitwa Galeedi (Gileadi); tena likaitwa Misipa (Chungulio), kwani alisema: Bwana na atuchungulie sisi, mimi na wewe, itakapokuwa, tusionane. Utakapowatesa hawa wanangu wa kike, au utakapochukua wake wengine kuliko hawa wanangu wa kike, kweli hakuna mtu shahidi huku kwetu sisi, lakini tazama, Mungu ni shahidi wetu sisi, mimi na wewe. Kisha Labani akamwambia Yakobo: Litazame chungu hili, litazame nalo hili jiwe, nililolisimika kuwa kielekezo chetu, mimi na wewe. Hili chungu na liwe shahidi, nacho hiki kielekezo kiwe ushuhuda wa kutukukataza, mimi nisilipite chungu hili kwenda kwako, wala wewe usilipite chungu hili kuja kwangu kufanya mabaya. Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Nahori aliye Mungu wa baba zao na atuamue! Ndipo, Yakobo alipoapa na kumtaja Mungu, baba yake Isaka aliyemcha. Kisha Yakobo akachinja hapo mlimani ng'ombe ya tambiko, akawaalika ndugu zake kuja kula naye; walipokwisha kula wakalala usiku huko mlimani. Kesho yake Labani akaamka na mapema, akanoneana na wanawe wa kiume na wa kike na kuwabariki; kisha Labani akaenda zake kurudi kwao. Yakobo alipokwenda safari yake akakutana na malaika wa Mungu. Yakobo alipowaona akasema: Hapa ndipo kambi la Mungu, akapaita mahali pale Mahanaimu (Makambi Mawili). Yakobo akatuma wajumbe kwenda katika nchi ya Seiri kwenye bara ya Edomu, wamtangulie kufika kwake mkubwa wake Esau. Akawaagiza kwamba: Hivi ndivyo, mmwambie bwana wangu Esau: Hivi ndivyo, mtumishi wako Yakobo anavyosema: Nimekaa ugenini kwake Labani, nikakawilia huko mpaka sasa, nikapata ng'ombe na punda, mbuzi na kondoo, watumwa wa kiume na wa kike, nikatuma kumpasha bwana wangu habari hizi, nijipatie upendeleo machoni pako. Hao wajumbe waliporudi kwake Yakobo akamwambia: Tumefika kwa mkubwa wako Esau, naye anakuja na watu 400, mkutane njiani. Ndipo, Yakobo alipoogopa sana na kusongeka moyoni, akawagawanya watu, aliokuwa nao, hata mbuzi na kondoo, nao ng'ombe na ngamia kuwa vikosi viwili, akasema: Esau atakapojia kikosi kimoja na kukishinda, hicho kingine kitakachosalia kitapata kupona. Kisha Yakobo akaomba: Mungu wa baba yangu Aburahamu na Mungu wa baba yangu Isaka, wewe Bwana umeniambia: Rudi katika nchi yako kwenye ndugu zako! Mimi nitakufanyizia mema. Hivyo, nilivyo mdogo, sipaswi na magawio yote wala na welekevu wote, uliomfanyizia mtumishi wako. Kwani hapo, nilipouvuka mto huu wa Yordani niliishika hii fimbo yangu tu, lakini sasa ni mwenye vikosi viwili. Niponye mkononi mwa mkubwa wangu Esau! Kwani namwogopa, asije, akanipiga mimi na wamama pamoja na wana. Wewe nawe umesema: Nitakufanyizia mema kweli, nao wa uzao wako nitawafanya kuwa wengi kama mchanga wa ufukoni usiohesabika kwa wingi. Kisha akalala huko usiku huo, akatoa katika yale mapato yaliyokuwa mkononi mwake matunzo ya kumpa kaka yake Esau: mbuzi majike 200 na madume 20, kondoo majike 200 na madume 20, ngamia wanyonyeshao 30 pamoja na wana wao, ng'ombe majike 40 na madume 10, punda majike 20 na wana wa punda 10; akawatia mikononi mwa watumwa wake, kundi kwa kundi peke yake, akawaambia hawa watumwa wake: Nitangulieni, tena katikati ya kila makundi mawili acheni nafasi. Naye wa kwanza akamwagiza kwamba: Mkubwa wangu Esau atakapokutana na wewe na kukuuliza kwamba: Wewe mtu wa nani? Unakwenda wapi? Nao hao nyama, wanaowatanguliza, ni wa nani? Umwambie: Ni wa mtumishi wako Yakobo, ndio matunzo, anayomtumia bwana wangu Esau, naye mwenyewe anatufuata nyuma. Naye wa pili na wa tatu nao wote waliowafuata watumwa hawa akawaagiza kwamba: Mtakapomwona Esau mwambieni maneno yayo hayo! Kisha semeni nanyi: Naye mtumishi wako Yakobo anatufuata nyuma. Kwani alisema moyoni mwake: Nitaupoza uso wake kwa hayo matunzo yatakayonitangulia; nitakapoonana naye halafu, labda atanipokea vema. Kwa hiyo matunzo yakamtangulia, naye akalala usiku huo humo kambini. Usiku huo alipoamka akawachukua wakeze wawili na wale vijakazi wawili na wanawe kumi na mmoja, akaenda kuvuka kivukoni kwa Yakobo; akawachukua, akawavusha hapo mtoni, akayavusha nayo yote, aliyokuwaa nayo. Naye Yakobo mwenyewe akasalia peke yake ng'ambo ya huko. Mara mtu akakamatana naye, mpaka jua lilipopambazuka. Alipoona, ya kuwa hamshindi Yakobo, akamgusa nyonga ya kiuno chake; ndipo, nyonga ya kiuno cha Yakobo ilipoteuka kwa kukamatana naye. Akamwambia Yakobo: Niache, niende zangu! Kwani jua limepambazuka. Lakini akasema: Sitakuacha, usiponibariki. Naye akamwuliza: Jina lako nani? Akasema: Yakobo. Ndipo, aliposema: Hutaitwa tena jina lako Yakobo, ila Isiraeli (Mshinda Mungu), kwani umeshindana na Mungu, hata na watu, ukawashinda. Naye Yakobo akamwuliza kwamba: Niambie jina lako! Akamwambia: Jina langu unaliulizia nini? Kisha akambariki hapo. Yakobo akapaita mahali pale Penieli (Uso wa Mungu) kwamba: Nimeonana na Mungu uso kwa uso, nayo roho yangu ikapona. Alipovuka hapo Penieli, usiku ukamchea, naye alikuwa akichechemea kwa ajili ya kiuno chake. Kwa sababu hii wana wa Isiraeli hawali mshipa ulio juu ya nyonga ya kiuno mpaka siku hii ya leo, kwani yule aliigusa nyonga ya kiuno cha Yakobo penye mshipa wa kiuno. Yakobo alipoyainua macho yake, atazame, mara akamwona Esau, akija pamoja na watu 400; ndipo, alipowagawanya watoto akimpa kila mama wake, Lea na Raheli na wale vijakazi wawili. Nao hao vijakazi na wana wao akawaweka mbele, akafuata Lea pamoja na wanawe, naye Raheli pamoja na Yosefu akawaweka nyuma. Naye mwenyewe akawatangulia, akajiangusha chini mara saba, mpaka amfikie mkubwa wake karibu. Ndipo, Esau alipomkibilia, akamkumbatia na kumwangukia shingoni, akamnonea, nao wote wawili wakalia machozi. Alipoyainua macho yake akawaona wale wanawake na watoto, akauliza: Hawa, ulio nao, ni wa nani? Akasema: Ndio watoto, Mungu aliompa mtumishi wako. Ndipo, wale vijakazi walipofika karibu pamoja na watoto wao na kumwangukia. Kisha Lea naye akafika karibu pamoja na watoto wake na kumwangukia, mwisho akaja Raheli pamoja na Yosefu na kumwangukia. Akauliza tena: Hicho kikosi chako chote, nilichokutana nacho, ni cha nini? Akasema: Ni kwamba, nijipatie upendeleo machoni pa bwana wangu. Esau akasema: Mimi ninazo mali nyingi, ndugu yangu; yashike yaliyo yako! Lakini Yakobo akajibu: Sivyo! Kama nimeona upendeleo machoni pako, yachukue matunzo haya mkononi mwangu! Kwa kuwa nilipouona uso wako, ikawa, kama nimeuona uso wake Mungu, maana umenipokea na kupendezwa. Sasa ipokee hiyo mbaraka, uliyoletewa! Kwani Mungu amenigawia mengi, nipate yote pia, nitoshewe. Ndivyo, aliyombembeleza, mpaka akiyachukua. Kisha akasema: Na tuondoke, twende zetu! Nami na nikutangulie. Lakini Yakobo akamwambia: Bwana wangu anajua, ya kuwa watoto hawa ni wachanga bado, tena ninao mbuzi na kondoo na ng'ombe wenye kunyonyesha, wao wakikimbizwa kwenda zaidi siku moja tu, kundi lote litakufa. Kwa hiyo bwana wangu na amtangulie mtumishi wake; mimi na nifuate poleple, kama hawa nyama, ninaowapeleka, wanavyoweza kwenda, hata nifike kwa bwana wangu huko Seiri. Ndipo, Esau aliposema: Nitakuachia watu wengine wa kwangu, nilio nao; lakini akasema: Wafanye nini? Inatosha, nikiona upendeleo machoni pa bwana wangu. Basi, Esau akarudi siku hiyohiyo na kuishika njia yake ya kwenda Seiri. Yakobo akaondoka kwenda Sukoti, akajijengea nyumba huko, nayo makundi yake akayajengea vibanda; kwa hiyo mahali pale pakaitwa Sukoti (Vibanda). Yakobo aliporudi kutoka Mesopotamia akafika na kutengemana kwenye mji wa Sikemu ulioko katika nchi ya Kanaani, akapiga kambi mbele yake huo mji. Akakinunua kile kipande cha shamba, alikolipiga hema lake, kwa wana wa Hamori, babake Sikemu, kwa fedha mia. Kisha akajenga huko pa kutambikia, akapaita Mungu Mwenyewe wa Isiraeli. Dina, binti Lea, ambaye alimzalia Yakobo, akatoka kuwatazama wanawake wa nchi hiyo. Sikemu, mwana wa Mhiwi Hamori aliyekuwa mkuu wa nchi hiyo, alipomwona akamchukua, akalala naye kwa kumtolea nguvu. Nayo roho yake ikagandamana naye Dina, binti Yakobo, akampenda huyu kijana, akasema naye maneno mazuri ya kuingia moyoni mwake huyu kijana. Kwa hiyo akamwambia baba yake Hamori kwamba: Niposee huyu mtoto, awe mke wangu. Yakobo aliposikia, ya kuwa yule amemchafua mwanawe Dina, wanawe waume walikuwa porini pamoja na makundi yake, kwa hiyo Yakobo akanyamaza kimya, mpaka wakirudi. Hamori, babake Sikemu, alipomtokea Yakobo kusema naye, wana wa Yakobo wakaja kutoka porini. Walipoyasikia hao waume wakaona uchungu na kukasirika sana, kwani aliwafanyia wao Waisiraeli upumbavu mbaya wa kulala na binti Yakobo; hilo ni jambo lisilofanywa. Hamori akasema nao kwamba: Roho yake mwanangu Sikemu inamtamani mtoto wenu, sasa mpeni, awe mkewe! Na mwoane na sisi mkitupa wana wenu wa kike, nao wana wetu wa kike mjichukulie! Na mkae nasi, nyo nchi hii na iwe wazi mbele yenu; kaeni tu na kuchuuzia huku, mjipatie huku mahali patakapokuwa penu. Naye Sikemu akamwambia babake Dina na ndugu zake: Afadhali nipate upendeleo machoni penu! Nayo mtakayoniambia nitawapa. Ijapo mtake mali nyingi sana za ukwe na matunzo mengi, nitawapa, kama mtakavyosema; nipeni tu kijana huyu kuwa mke wangu! Ndipo, wana wa Yakobo walipomjibu Sikemu na baba yake Hamori kwa udanganyifu, kwa kuwa alimchafua umbu lao Dina; kwa hiyo wakasema na kuwaambia: Hatuwezi kulifanya jambo hili, tumpe mtu mwenye govi umbu letu, kwani hivi vitatutia soni. Tutaweza kuwaitikia neno hilo hapo tu, mtakapokuwa kama sisi, kwenu wa kiume wote wakitahiriwa. Ndipo, tutakapowapa wana wetu wa kike, tujichukulie nao wana wenu wa kike, tukae pamoja nanyi kuwa kabila moja. Lakini msipotusikia na kutahiriwa, tutamchukua mtoto wetu, twende zetu. Haya maneno yao yakawa mema machoni pake Hamori napo machoni pake Sikemu, mwana wa hamori. Huyu kijana hakukawa kulifanya neno hilo, kwani alipendezwa naye binti Yakobo; naye alikuwa mwenye macheo kuliko wote a mlango wa baba yake. Hamori na mwanawe Sikemu walipofika langoni pa mji wao wakasema na watu wa mji wao kwamba: Watu hawa wanataka kukaa kwetu katika nchi yetu na kutengemana, wachuuzie huku; nanyi mnaiona nchi hii kuwa pana huku na huko, waenee nao; wana wao wa kike tutajichukulia kuwa wake zetu, nao wana wetu wa kike tutawapa wao. Lakini liko neno moja, watu hawa wanalolitaka, wapate kutuitikia na kukaa kwetu, tuwe kabila moja, ni hili: Kwetu wa kiume wote watahiriwe, kama wenyewe walivyotahiriwa. Je? Hivyo makundi yao na mapato yao na nyama wote, wanaowafuga, hawatakuwa mali zetu sisi? Kwa hiyo na tuwaitikie, wakae kwetu! Wote waliotoka langoni pa mji wakamsikia Hamori na mwanawe Sikemu, wakatahiriwa wa kiume wote pia, ndio wao wote waliotoka langoni pa mji wake. Ikawa siku ya tatu, walipokuwa wanaumwa sana, wana wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, ndugu zake Dina, wakachukua kila mtu upanga wake, wakaingia mle mjini, watu walimokaa na kutulia, wakawaua wa kiume wote. Naye Hamori na mwanawe Sikemu wakawaua kwa ukali wa panga, kisha wakamchukua Dina nyumbani mwa Sikemu, wakatoka kwenda zao. Ndipo, wana wengine wa Yakobo walipowajia wale waliouawa, wakaziteka mali za humo mjini, kwa kuwa walimchafua umbu lao. Wakawachukua mbuzi na kondoo wao na ng'ombe wao na punda wao nayo yaliyokuwamo mjini nayo yaliyokuwako mashambani. Wakateka mali zao zote na wana wao wote na wake zao, nayo yote yaliyokuwamo nyumbani wakayanyang'anya. Naye Yakobo akamwambia Simeoni na Lawi: Mmenipatia mabaya, mmefanya mnuko wangu kuwa mbaya kwao wanaokaa katika nchi hii, kwa Wakanaani na Waperizi, nami watu wangu wanahesabika upesi. Watakaponikusanyikia, watanipiga; ndivyo, nitakavyotoweka mimi na mlango wangu. Lakini wakasema: Je? Tungeacha tu, amtumie umbu letu kama mwanamke mgoni? Mungu akamwambia Yakobo: Inuka, upande kwenda Beteli kukaa huko! Tena jenga huko pa kumtambikia Mungu aliyekutokea huko, ulipomkimbia kaka yako Esau! Ndipo, Yakobo alipowaambia wao wa mlango wake nao wote, aliokuwa nao: Iondoeni miungu migeni iliyo kwenu bado! Kisha jieueni na kuvaa nazo nguo nyingine! Kisha na tuondoke, tupande kwenda Beteli, nijenge huko pa kumtambikia Mungu aliyeniitikia siku ile, nilipokuwa nimesongeka, akawa pamoja na mimi katika safari hiyo, niliyokwenda. Ndipo, walipompa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, nayo mapete ya masikioni mwao, naye Yakobo akayafukia chini ya mkwaju uliokuwa karibu ya Sikemu. Walipoondoka, kitisho cha Mungu kikaiguia ile miji yote iliyowazunguka, wasiwakimbize wana wa Yakobo na kuwafuata. Ndivyo, yakobo alivyofika Luzi katika nchi ya Kanaani, ndio Beteli, yeye pamoja na watu wote, aliokuwa nao. Akajenga huko pa kutambikia, akapaita mahali pale Mungu wa Beteli, kwani ndiko, Mungu alikomtokea, alipomkimbia kaka yake. Siku zile akafa Debora aliyekuwa yaya wake Rebeka, akazikwa upande wa chini hapo Beteli chini ya mvule, nao ukaitwa Mvule wa Maombolezo. Mungu akamtokea Yakobo tena, aalipokwisha kurudi Mesopotamia, akambariki. Hapo Mungu akamwambia: Jina lako ni Yakobo, lakini usiitwe tena jina lako Yakobo, ila jina lako liwe Isiraeli! Kwa hiyo wakamwita Isiraeli. Kisha Mungu akamwambia: Mimi ni Mungu Mwenyezi; na uzae wana, upate kuwa wengi, taifa na kundi zima la mataifa litatoka kwako, nao wafalme watatoka kiunoni mwako. Nayo nchi hii, niliyompa Aburahamu na Isaka, nakupa wewe nawe, nao wa uzao wako wajao nyuma yako nitawapa nchi hii. Kisha Mungu akapaa juu na kutoka kwake mahali hapo, aliposema naye. Mahali hapo, aliposema naye, Yakobo akapasimamisha nguzo, nayo nguzo hiyo ilikuwa ya mawe, akaimwagia kinywaji cha tambiko, kisha akaipaka mafuta juu yake. Yakobo akapaita jina lake mahali hapo, Mungu aliposema naye, Beteli. Kisha wakaondoka Beteli. Ikawa, uliposalia mwendo wa kipande kifupi tu kufika Efurata, Raheli akazaa, nako huko kuzaa kwake kukawa kugumu. Hapo, machungu yake ya kuzaa yalipozidi, mzalishaji akamwambia: Usiogope! Kwani nayo mara hii utazaa mtoto mume. Ikawa roho yake ilipomtoka kwa kupatwa na kufa, akamwita jina lake Benoni (Azimalizaye nguvu zangu), lakini baba yake akamwita Benyamini (Mbahati). Ndivyo, Raheli alivyokufa, akazikwa hapohapo penye njia ya kwenda Efurata, ndio Beti-Lehemu. Yakobo akasimamaisha juu ya kaburi lake nguzo ya mawe, nayo nguzo hiyo iko juu ya kaburi la Raheli hata siku ya leo. Kisha Isiraeli akaondoka, akalipiga hema lake ng'ambo ya huko ya mnara wa Ederi. Ikawa, Israeli alipokaa katika nchi ile, Rubeni akaenda, akalala na Biliha, suria ya baba yake; naye Isiraeli akavisikia. Wana wa Yakobo walikuwa kumi na wawili. Wana wa Lea ni wanawe wa kwanza wa Yakobo: Rubeni, tena Simeoni na Lawi na Yuda na Isakari na Zebuluni. Wana wa Raheli ni Yosefu na Benyamini. Nao wana wa Biliha, kijakazi wake Raheli, ni Dani na Nafutali. Nao wana wa Zilpa, kijakazi wake Lea, ni Gadi na Aseri. Hawa ndio wana wa Yakobo, aliozaliwa huko Mesopotamia. Kisha Yakobo akafika kwa baba yake Isaka kule Mamure karibu ya Kiriati-Arba, ndio Heburoni, aburahamu na Isaka walikokaa ugenini. Nazo siku zake Isaka zilikuwa miaka 180. Ndipo, Isaka alipozimia, akafa, akachukuliwa kwenda kwao walio wa ukoo wake; naye alikuwa mkongwe mwenye siku za kushiba siku za kuwapo. Kisha wanawe Esau na Yakobo wakamzika. Hivi ndivyo vizazi vyake Esau aliyeitwa Edomu: Esau akachukua wakeze kwao wanawake wa Kanaani: Ada, binti Mhiti Eloni, na Oholibama, binti Ana, binti Mhiwi Siboni, na Basimati, binti Isimaeli, umbu lake Nebayoti. Ada akamzalia Esau Elifazi, naye Basimati akamzaa Reueli. Naye Oholibama akamzaa Yeusi na Yalamu na Kora. Kisha Esau akawachukua wakeze na wanawe wa kiume na wa kike nao wote waliokuwa nyumbani mwake na mbuzi na kondoo wake na nyama wengine wote, aliowafuga, na mapato yake yote, aliyoyapata katika nchi ya Kanaani, akaondoka kwa ndugu yake Yakobo, akaenda katika nchi nyingine. Kwani mapato yao yalikuwa mengi, wasiweze kukaa pamoja; nayo nchi hiyo, waliyoikaa ugeni, haikuweza kuwaeneza kwa ajili ya makundi yao. Kwa hiyo Esau akaenda kukaa vilimani kwa Seiri, naye Esau ndiye Edomu. Navyo hivi ndivyo vizazi vyake Esau, baba yao Waedomu, milimani kwa Seiri. Haya ndiyo majina yao wanawe Esau: Elifazi, mwana wa Ada, mkewe Esau, tena Reueli, mwana wa Basimati, mkewe Esau. Nao wana wa Elifazi walikuwa Temani, Omari, Sefo na Gatamu na Kenazi. Naye Timuna alikuwa suria yake Elifazi, mwana wa Esau; akamzalia Elifazi Amaleki. Hawa ndio wana wa Ada, mkewe Esau. Nao hawa ndio wana wa Reueli: Nahati na Zera, Sama na Miza; hawa ndio wana wa Basimati, mkewe Esau. Nao hawa ndio wana wa Oholibama, binti Ana, binti Siboni, mkewe Esau, aliomzalia Esau: Yeusi na Yalamu na Kora. Hawa ndio majumbe wao wana wa Esau: Wana wa Elifazi, mwanawe wa kwanza wa Esau, walikua: Jumbe Temani, jumbe Omari, jumbe Sefo, jumbe Kenazi, jumbe Kora, jumbe Gatamu, jumbe Amaleki. Hawa ndio majumbe wa Elifazi katika nchi ya Edomu, nao ndio wana wa Ada. Nao hawa ndio wana wa Reueli, mwana wa Esau: Jumbe Nahati, Jumbe Zera, Jumbe Sama, jumbe Miza. Hawa ndio majumbe wa Reueli katika nchi ya Edomu, nao ndio wana wa Basimati, mkewe Esau. Nao hawa ndio wana wa Oholibama, mkewe Esau: Jumbe Yeusi, jumbe Yalamu, jumbe Kora. Hawa ndio majumbe wa Oholibama, binti Ana, mkewe Esau. Hawa ndio wanawe Esau, nao ndio majumbe wao. Hawa ndio Waedomu. Hawa ndio wana wa Mhori Seiri waliokuwa katika hiyo nchi: Lotani na Sobali na Siboni na Ana, na Disoni na Eseri na Disani; hawa ndio majumbe wa Wahori, wana wa Seiri, katika nchi ya Edomu. Nao wana wa Lotani walikuwa Hori na Hemamu, naye umbu lake Lotani ni timuna. Nao hawa ndio wana wa Sobali: Alwani na Manahati na Ebali, Sefo na Onamu. Nao hawa ndio wana wa Siboni: Aya na Ana; huyu Ana ndiye aliyeziona chemchemi za maji ya moto nyikani alipowachunga punda wa baba yake Siboni. Nao hawa ndio wana wa Ana: Disoni na Oholibama, binti Ana. Nao hawa ndio wana wa Disoni: Hemudani na Esibani na Itirani na Kerani. Hawa ndio wana wa Eseri: Bilihani na Zawani na Akani. Hawa ndio wana wa Disani: Usi na Arani. Hawa ndio majumbe wa Wahori: Jumbe Lotani, jumbe Sobali, jumbe Siboni, jumbe Ana, jumbe Disoni, jumbe Eseri, jumbe Disani; hawa ndio majumbe wa Wahori walioushika ujumbe wao katika nchi ya Seiri. Nao hawa ndio wafalme waliotawala katika nchi ya Edomu, wana wa Isiraeli walipokuwa hawajapata bado mfalme. Bela, mwana wa Beori, alikuwa mfalme huko Edomu, nalo jina la mji wake ni Dinihaba. Bela alipokufa, Yobabu, mwana wa Zera aliyetoka Bosira, akawa mfalme mahali pake. Yobabu alipokufa, Husamu wa nchi ya Watemani akawa mfalme mahali pake. Husamu alipokufa, Hadadi, mwana wa Bedadi aliyewapiga Wamidiani katika mbuga za Wamoabu, akawa mfalme mahali pake; nalo jina la mji wake ni Awiti. Hadadi alipkufa, Samula aliyetoka Masireka akawa mfalme mahali pake. Samula alipokufa, Sauli aliyetoka Rehoboti wa Mtoni akawa mfalme mahali pake. Sauli alipokufa, Baali-Hanani, mwana wa Akibori, akawa mfalme mahali pake. Baali-Hanani, mwana wa Akibori, alipokufa, Hadari akawa mfalme mahali pake, nalo jina la mji ni Pau, nalo jina la mkewwe ni Mehetabeli, binti Matiredi, binti Mezahabu. Haya ndiyo majina ya majumbe wa Esau, tena ndivyo, walivyoitwa majina yao kwa ndugu zao napo mahali pao, walipokaa: Jumbe Timuna, jumbe Alwa, jumbe Yeteti, jumbe Oholibama, jumbe Ela, jumbe Pinoni, jumbe Kenazi, jumbe Temani, jumbe Mibusari, jumbe Magidieli, jumbe Iramu. Hawa ndio majumbe wa Waedomu, jinsi walivyoitwa kwa koo zao katika hizo nchi, walizozichukua kuwa zao. Huyu ndiye Esau, baba yao Waedomu. Yakobo akakaa katika nchi hiyo, baba yake alikokaa ugenini, ndio nchi ya Kanaani. Hivi ni vizazi vya Yakobo: Yosefu alipopata miaka 17, akachunga mbuzi na kondoo pamoja na kaka zake; huyu kijana Yosefu alipokuwa pamoja na wana wa Biliha nao wana wa Zilpa, wakeze baba yake, yeye Yosefu akamsimulia baba yao mambo yao mabaya. Naye Isiraeli alimpenda Yosefu kuliko wanawe wote, kwa kuwa ni mwanawe wa uzee wake; kwa hiyo akamshonea kanzu ya nguo za rangi. Kaka zake walipoona, ya kuwa baba yao alimpenda kuliko ndugu zake, wakamchukia, hawakuweza kusema naye kwa upole. Kisha Yosefu akaota ndoto, akawasimulia kaka zake; ndipo, walipozidi kumchukia, kwani aliwaambia: Isikieni ndoto hii, niliyoiota! Nimeona, sisi tulikuwa shambani tukifunga miganda; mara mganda wangu ukainuka, ukasimama, nayo miganda yenu ikauzunguka, ikazungukia mganda wangu. Ndipo, kaka zake walipomwambia: Je? Unataka kuwa mfalme wetu, ututawwale? Wakazidi kumchukua sana kwa ajili ya ndoto zake na kwa ajili ya maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akaisimulia nayo kaka zake akiwaambia: Tazameni! Nimeota ndoto nyingine, nikaona, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikiniangukia. Alipomsimulia baba yake nao kaka zake ndoto hizi, baba yake akamkemea, akamwambia: Hiyo ndoto yako, uliyoiota, ni ndoto gani? Je? mimi na mama yako na kaka zako tuje, tukuangukie chini? Ndipo, kaka zake walipomwonea wivu, lakini baba yake akayashika maneno hayo na kuyaangalia. Kisha kaka zake walipokwenda kuwachnga mbuzi na kondoo wa baba yao huko Sikemu, Isiraeli akamwambia Yosefu: Kumbe kaka zako hawako Sikemu wakichunga mbuzi na kondoo? Haya! Nikutume kwenda kwao! Akamwitikia: Mimi tayari. Akamwambia: Nenda kuwatazama kaka zako, kama hawajambo, nao mbuzi na kondoo, kama hawajambo! Kisha uniletee habari! Akamtuma kutoka bondeni kwa Heburoni kwenda Sikemu. Ndipo, mtu alipomwona, alipokuwa amepotelewa na njia porini, naye yule mtu akamwuliza: Unatafuta nini? Akasema: Ninawatafuta kaka zangu; niambie, wanakochungia mbuzi na kondoo! Yule mtu akasema: Wameondoka huku, kwani naliwasikia, wakisema: Na twende Dotani! Basi, Yosefu alipowafuata kaka zake akawaona Dotani. Nao walipomwona, angaliko mbali, wakafanya shauri la kumwua, alipokuwa hajafika kwao, wakasemezana: Mtazameni Chandoto! Huyu, anakuja! Sasa haya! na tumwue! Kisha tumtupe shimoni mo mote, tuseme: Nyama mkali amemla! Ndipo, tutakapoona, ndoto zake zitakavyotimia. Rubeni alipoyasikia alitaka kumponya mikononi mwao, akawaambia: Tusimwue! Kisha Rubeni akawaambia: Msimwage damu yake! Mtupeni humu shimoni huku nyikani! Lakini msimwue kwa kumpelekea mikono! Naye alisema hivyo, apate kumponya mikononi mwao, amrudishe kwa baba yake. Ikawa, Yosefu alipofika kwa kaka zake, wakamvua kanzu yake, maana aliivaa ile kanzu ya nguo za rangi; kisha wakamchukua, wakamtumbukiza katika shimo, nalo hilo shimo lilikuwa halina maji. Kisha wakakaa, wale chakula. Walipoyainua macho yao kutazama, mara wakaona msafara wa Waisimaeli waliotoka Gileadi wenye ngamia waliochukua manukato na mafuta ya mkwaju na uvumba, nao walikwenda kuvipeleka Misri. Ndipo, Yuda alipowaambia ndugu zake: Haifai, tukimwua ndugu yetu na kuificha damu yake; haya! na tumwuze kwa hawa Waisimaeli, tusimpige kwa mikono yetu! Kwani ni ndugu yetu, tuliyezaliwa naye. Nao ndugu zake wakamwitikia. Basi, hao wachuuzi wa Midiani walipopita, wakamwopoa Yosefu na kumtoa mle shimoni, wakamwuza Yosefu kwao hao Waisimaeli kwa fedha 20, nao wakampeleka Yosefu Misri. Rubeni aliporudi hapo shimoni, akaona, ya kama Yosefu hayumo; ndipo, alipozirarua nguo zake, akarudi kwa ndugu zake, akawaambia: Mtoto hayumo, mimi nami niende wapi? Kisha wakaichukua kanzu ya Yosefu, wakachinja dume la mbuzi, wakaichovya hiyo kanzu katika damu yake. Kisha wakaituma hiyo kanzu ya nguo za rangi kumpelekea baba yao, wakamwambia: Nguo hii tumeiokota; itazame, kama ndiyo kanzu ya mwanao, au kama siyo! Akaitambua, akasema: Ni kanzu ya mwanangu! Nyama mkali amemla, Yosefu ameraruliwa kweli! Ndipo, Yakobo alipozirarua nguo zake, akavaa gunia kiunoni, akamwombolezea mwanawe siku nyingi. Wakainuka wanawe wote wa kiume nao wote wa kike, wamtulize moyo, lakini akakataa kutulizwa moyo akisema: Nitashuka mwenye ukiwa huko kuzimuni, mwanangu aliko. Ndivyo, baba yake alivyomlilia. Wale Wamidiani wakamwuza huko Misri kwa Potifari aliyekuwa mtumishi wa nyumbani mwa Farao na mkuu wao waliomlinda Farao. Ikawa wakati huo, ndipo, Yuda alipoondoka kwa ndugu zake, akajiunga na mtu wa Adulamu, jina lake Hira. Huko Yuda akaona binti Mkanaani, jina lake sua, akamchukua, akaingia kwake. Naye akapata mimba, akazaa mtoto mume; jina lake yule akamwita Eri. Alipopata mimba tena akazaa mtoto mume, akamwita jina lake Onani. Akendelea, akazaa tena mtoto mume, akamwita jina lake Sela. Naye Yuda alikuwa huko Kizibu, alipomzaa. Yuda akamwoza mwanawe wa kwanza Eri, jina lake mkewe ni Tamari. Lakini Eri, mwana wa kwanza wa Yuda, akawa mbaya machoni pa Bwana, kwa hiyo Bwana akamwua. Ndipo, Yuda alipomwambia Onani: Ingia kwa mkewe kaka yako, umsimikie unyumba naye na kumpatia kaka yako mzao kwake! Kwa kuwa Onani alijua, ya kama huyo mzao hatakuwa wake yeye, basi, kila mara alipoingia kwa mkewe kaka yake kwanza akaziangusha mbegu zake chini, asimpatie kaka yake uzao. Hayo, aliyoyafanya, yakawa mabaya machoni pa Bwana, kwa hiyo akamwua naye. Ndipo, Yuda alipomwambia mkwewe Tamari: Kaa tu na ujane wako nyumbani mwa baba yako, hata mwanangu Sela akue! Kwani alisema moyoni, asife huyu naye kama kaka zake. Kwa hiyo Tamari akaenda, akakaa nyumbani mwa baba yake. Siku zilipopita nyingi, binti Sua, mkewe Yuda, akafa. Yuda alipokwisha kujituliza moyo kwa ajili ya kufa kwake akapanda kwenda Timunati kwao waliowakata kondoo wake manyoya, yeye na rafiki yake Hira wa Adulamu. Tamari alipopashwa habari kwamba: Tazama, mkweo anapanda kwenda Timunati kuwakata kondoo wake manyoya, akayavua mavazi yake ya ujane, akajifunika kwa ukaya na kujitandia nguo, kisha akakaa hapo pa kuingilia Enaimu kwenye njia ya timunati, kwani aliona, ya kuwa Sela amekwisha kukua, lakini yeye hakuozwa naye, awe mkewe. Yuda alipomwona akamwazia kuwa mwanamke mgoni, kwani alijifunika ushungi, akamgeukia na kumwendea hapo njiani, alipokaa, akamwambia: Acha, niingie kwako! kwani hakumjua kuwa mkwewe. Akamwuliza: Utanipa nini ukiingia kwangu? Akasema: Mimi nitakuletea dume la mbuzi, nitakayemtoa mle makundini; naye akamwambia: Nipe rehani, niishike, mpaka utakapomleta! Akamwuliza: Nikupe rehani gani? Akamwambia: Pete yako yenye muhuri na mshipi wako na fimbo yako, unayoishika mkononi. Akampa, kisha akaingia kwake, naye akapata mimba. Alipoinuka kwenda zake, akaondoa ukaya wake usoni pake, akayavaa mavazi yake ya ujane. Yuda alipotuma dume la mbuzi mkononi mwa rafiki yake wa Adulamu, achukue nazo zile rehani mkononi mwa yule mwanamke, hakumwona. Naye alipowauliza watu wa mahali hapo kwamba: Yuko wapi yule mwanamke mgoni wa patakatifu aliyekaa njiani hapo Enaimu? Wakamwambia: Huku hakuwako mwanamke mgoni wa patakatifu. Akarudi kwake Yuda, akamwambia: sikumwona, nao watu wa mahali pale wanasema: Huku hakuwako mwanamke mgoni wa patakatifu. Ndipo, Yuda aliposema: Na ajitwalie, tusije kutwezwa! Tazama, nimempeleka huyu dume la mbuzi, nawe hukumwona! Miezi mitatu ilipopita, Yuda akapashwa habari kwamba: Mkweo Tamari amefanya ugoni, naye akapata mimba kwa huo ugoni. Ndipo, Yuda aliposema: Mtoeni, ateketezwe! Alipotolewwa akatuma kwa mkwewe kwamba: Mimi nimepata mimba kwake yeye aliye mwenye vitu hivi; akaendelea kusema: Mtambue mwenye pete hii yenye muhuri na mwenye mshipi huu na mwenye fimbo hii! Yuda alipovitambua vitu hivyo akasema: Yeye ni mwongofu kuliko mimi; ameyafanya, kwa kuwa sikumpa mwanangu Sela. Lakini hakumjua tena hata mara moja. Siku zake za kuzaa zilipotimia, wakaona ya kuwa tumboni mwake wamo wana wa pacha. Ikawa, alipozaa, mmoja akatoa mkono; ndipo mzalishaji alipomfunga mkononi pake uzi mwekundu kwamba: Huyu ametoka wa kwanza. Lakini ikawa, alipourudisha mkono wake, mara ndugu yake akatoka; ndipo, aliposema: Kumbe umejipasulia ufa namna hii! Kwa hiyo wakamwita jina lake Peresi (Ufa). Kisha ndugu yake akatoka naye mwenye uzi mwekundu mkononi pake, kwa hiyo wakamwita jina lake Zera (Mwekundu). Yosefu alipopelekwa Misri, Potifari aliyekuwa mtumishi wa nyumbani mwa Farao na mkuu wao waliomlinda Farao akamnunua mikononi mwao wale Waisimaeli waliompeleka huko. Bwana akawa naye Yosefu, kwa hiyo akafanikiwa alipokuwa nyumbani mwa bwana wake wa Kimisri. Bwana wake alipoona, ya kuwa Bwana yuko pamoja naye, nayo yote, anayoyafanya, Bwana anayafanikisha mikononi mwake, Yosefu akaona upendeleo machoni pake, akampa kumtumikia mwenyewe, kisha akamweka kuisimamia nyumba yake yote, nayo yote, aliyokuwa nayo, akayatia mkononi mwake. Tangu hapo, alipomweka nyumbani mwake kuyasimamia yote, aliyokuwa nayo, Bwana akaibariki nyumba ya huyu Mmisri kwa ajili yake Yosefu; mbaraka ya Bwana ikayakalia yote yaliyokuwa yake nyumbani na shambani. Kwa hiyo akamwachia Yosefu yote, aliyokuwa nayo, yawe mkononi mwake, naye mwenyewe hakujua chake cho chote, isipokuwa chakula chake, alichokila. Naye Yosefu alikuwa mzuri wa umbo na wa uso. Siku zilipopita, mkewe bwana wake akamtupia Yosefu macho, akamwambia: Lala kwangu! Lakini akakataa, akamwambia mkewe bwana wake: Tazama! Bwana wangu hajui cho chote kilichomo humu nyumbani, ninachokiangalia, nayo yote, aliyo nayo, ameyatia mkononi mwangu. Humu nyumbani hamna mkubwa kuliko mimi, wala hamna kitu, alichonikataza, ni wewe peke yako, kwa kuwa wewe ndiwe mkewe. Kwa hiyo nitawezaje kufanya kibaya kilicho kikuu kama hiki nikimkosea Mungu? Hivi ndivyo, alivyomwambia Yosefu siku kwa siku, lakini Yosefu hakumwitikia kulala naye wala kuwa pamoja naye. Ikawa siku moja, alipoingia kufanya kazi zake chumbani, msimokuwa na mtu hata mmoja wao wakazi wa humo chumbani, ndipo, alipomkamata nguo yake na kusema: Lala kwangu! Lakini akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia na kutoka nje. Ikawa, alipoona, ya kuwa ameiacha nguo yake mkononi mwake na kukimbia kwenda nje, akawaita waliomo nyumbani, akawaambia kwamba: Tazameni! Ametuletea huyu Mwebureo wa kucheza na sisi! Ameingia mwangu kulala na mimi, lakini nikapiga kelele kubwa. Naye aliposikia, ya kama nimezipaza sauti zangu za kuita watu, akaiacha nguo yake kwangu, akakimbia kwenda nje. Akaiweka nguo yake kwake, hata bwana wake arudi nyumbani mwake. Ndipo, alipomwambia maneno yayo hayo ya kwamba: Yule mtumwa Mwebureo, uliyemleta kwetu kucheza na sisi, ameingia mwangu. Lakini nilipozipaza sauti zangu za kuita watu, akaiacha nguo yake kwangu, akakimbia kwenda nje. Ikawa, bwana wake alipoyasikia haya maneno ya mkewe, aliyomwambia ya kwamba: Mtumwa wako amenifanyia haya na haya, akakasirika na kuwaka moto. Ndipo, bwana wake Yosefu alipomchukua, akamfunga kifungoni mle chumbani, mlimokuwa na wafungwa wa mfalme; humo kifungoni ndimo, Yosefu alimotiwa. Lakini Bwana alikuwa naye Yosefu, akamtolea utu na kumpatia upendeleo machoni pa mkuu wa kifungo. Huyu mkuu wa kifungo akatia mkononi mwa Yosefu wafungwa wote waliokuwamo mle kifungoni, yote waliyoyafanya humo yawe kazi yake yeye. Katika yote, mkuu a kifungo aliyoyatia mkononi mwake, hakikuwamo cho chote, alichokitazama mwenyewe, kwa kuwa Bwana alikuwa na Yosefu, nayo yote aliyoyafanya Bwana akayafanikisha. Ikawa, mambo hayo yalipomalizika, mkuu wa watunza vinywaji vya mfalme wa Misri na mkuu wa wachoma mikate wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri. Naye Farao akawakasirikia hawa watumishi wake wawili wa nyumbani mwake, Yule mkuu wa watunza vinywaji naye mkuu wa wachoma mikate. Akawafunga, waangaliwe kifungoni katika nyumba ya mkuu wao waliomlinda mfalme; ndimo, Yosefu alimokuwa naye kwa kufungwa. Naye mkuu wao waliomlinda mfalme akamweka Yosefu kuwaangalia na kuwatumikia, wakawamo hizo siku wakiangaliwa. Usiku mmoja wote wawili wakaota ndoto, kila mtu ndoto yake yenye maana yake, yule mtunza vinywaji vya mfalme naye yule mchoma mikate ya mfalme wa Misri waliokuwa wamefungwa kifungoni. Yosefu alipoingia asubuhi chumbani mwao, awatazame, akawaona, ya kuwa wamenuna, akawauliza hawa wafungwa wa Farao walioangaliwa naye katika nyumba ya bwana wake kwamba: Mbona leo nyuso zenu ni mbaya? Wakamwambia: Tumeota ndoto, lakini mwenye kuzifumbua hakuna. Yosefu akawaambia: Kumbe kufumbua siko kwake Mungu? Lakini nisumulieni! Mkuu wao watunza vinywaji akamsimulia ndoto yake, akamwambia: Katika ndoto yangu nimeona machoni pangu mzabibu; katika mzabibu huu yalikuwamo matawi matatu, nao ulipochipuka, ukachanua maua yake, navyo vichala vyake vikaivisha zabibu. Nacho kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazishika zile zabibu, nikazikamulia katika kikombe cha Farao, kisha nikampa Farao, hicho kikombe mkononi mwake. Yosefu akamwambia: Maana yake ndio hii: hayo matawi matatu ndio siku tatu; siku tatu zitakapopita, Farao atakupa kukiinua kichwa chako, kwani atakurudisha katika kazi yako, umpe kikombe chake Farao mkononi mwake, kama ilivyokupasa kale, ulipokuwa mtunza vinywaji vyake. Lakini utakapopata mema sharti unikumbe na kunihurumia ukiniombea kwake Farao, anitoe humu nyumbani. Kwani nimekwibwa katika nchi ya Waebureo, huku nako sikukosa lo lote, wakanitia humu kifungoni. Mkuu wa wachoma mikate alipoona, ya kuwa amefumbua vema, akamwambia Yosefu: Mimi nami katika ndoto yangu nimejiona, nilipokuwa nimechukua nyungo tatu zenye vikate vyeupe kichwani pangu. Namo katika ungo wa juu vilikuwamo vikate vizuri vyo vyote vya Farao, wachoma mikate wanavyovitengeneza, nao ndege wakavila mwenye ungo kichwani pangu. Yosefu akajibu akisema: Maana yake ndio hii: hizo nyungo tatu ndio siku tatu; siku tatu zitakapopita, Farao atakupa kukiinua kichwa chako, kiwe juu yako zaidi, atakunyonga katika mti, nao ndege watazila nyama za mwili wako. Siku ya tatu ikawa siku ya kuzaliwa kwake Farao; ndipo, alipowaandalia watumishi wake wote karamu; hapo katikati ya watumishi wake akampa mkuu wa watunza vinywaji naye mkuu wa wachoma mikate kuviinua vichwa vyao, akimrudisha mkuu wa watunza vinywaji katika kazi yake ya kutunza vinywaji, ampe Farao kikombe mkononi mwake, naye mkuu wa wachoma mikate akamnyonga, kama Yosefu alivyowafumbulia ndoto. Lakini mkuu wa watunza vinywaji hakumkumbuka Yosefu, akamsahau. Miaka miwili ilipopita, Farao akaota, akajiona, akisimama kando ya mto. Akaona, ng'ombe saba wazuri mno walionona wakitoka mtoni, wakapanda kwenda kula majanini. Kisha akaona, ng'ombe saba wengine wakitoka mtoni kuwafuata wale, ni wabaya mno wenye nyama kavu, wakaenda kusimama kando yao wale ng'ombe wa kwanza ukingoni kwa mto. Kisha hawa ng'ombe wabaya wenye nyama kavu wakawala wale ng'ombe saba wazuri walionona; ndipo, Farao alipoamka. Alipolala tena usingizi akaota mara ya pili, akaona, masuke saba yaliyo manene na mazuri yakitoka katika bua moja. Kisha akaona, masuke saba mengine yakichipuka nyuma yao, nayo ni membamba kwa kunyaushwa na upepo wenye joto. Haya masuke membamba yakayameza yale masuke manene yaliyojaa ngano. Ndipo, Farao alipoamka, akaona, ya kuwa ameota. Kulipokucha akahangaika rohoni, akatuma kuwaita waaguaji wote walioko Misri na wajuzi wote wa ndoto; lakini Farao alipowasimulia ndoto zake, hakupatikana aliyemfumbulia Farao maana ya hizo ndoto. Ndipo, mkuu wa watunza vinywaji alipomwambia Farao kwamba: Leo hivi ninayakumbuka makosa yangu. Farao alipowakasirikia watumishi wake, alinitia katika kifungo nyumbani mwake mkuu wao wanaomlinda mfalme, mimi pamoja na mkuu wa wachoma mikate; ndipo, tulipoota ndoto usiku mmoja mimi na yeye, tulikuwa tumeota kila mtu ndoto yake yenye maana yake yeye. Basi, mle tulikuwa na kijana wa Kiebureo, mtumwa wake mkuu wao wanaomlinda mfalme; tulipomsimulia ndoto zetu, akamfumbulia maana yao, kila mtu akamfumbuli ndoto yake yeye. Navyo, alivyotufumbulia, vikawa hivyo; mimi walinirudisha katika kazi, naye mwenzangu akanyongwa. Ndipo, Farao alipotuma kumwita Yosefu; wakamfungua upesi mle kifungoni, akajinyoa nywele, akavaa nguo nyingine, kisha akaja kuingia kwake mfalme. Farao akamwambia Yosefu: Nimeota ndoto, lakini hakuna anayezifumbua. Nimesikia habari yako kwamba: Unaposikia ndoto huifumbua. Yosefu akamjibu Farao kwamba: Sio mimi, Mungu na ayafunue yatakayompatia Farao utengemano! Ndipo, Farao alipomwambia Yosefu: Katika ndoto yangu nimejiona, nikisimama ukingoni kwa mto. Mara nikaona, ng'ombe saba wazuri mno walionona wakitoka mtoni, wakapanda kwenda kula majanini. Kisha nikaona, ng'ombe saba wengine wakitoka mtoni kuwafuata wale, ni wenye kukonda kuwa wabaya sanasana kwa kuwa wenye nyama kavu; katika nchi zote za Misri sijaona bado ng'ombe wabaya kama hao. Hao ng'ombe wabaya waliokonda hivyo wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza walionona. Hao walipoingia tumboni mwao, haikujulikana, ya kuwa wamo tumboni mwao; nilipowatazama, walikuwa wabaya kama hapo kwanza. Ndipo, nilipoamka. Nilipoota tena nikaona, masuke saba yaliyojaa ngano kuwa mazuri yakitoka katika bua moja. Kisha nikaona masuke saba yaliyochipuka nyuma yao, nayo ni matupu na membamba kwa kunyaushwa na upepo wenye joto. Hayo masuke membamba yakayameza yale masuke mazuri. Nami nikawaambia waaguaji hizi ndoto, lakini hakuna anayeweza kuniambia maana. Ndipo, Yosefu alipomwmbia Farao: Ndoto za Farao ni moja; Mungu amemjulisha Farao atakayoyafanya. Ng'ombe saba wazuri ndio miaka saba, nayo masuke saba mazuri ndio miaka saba; ndoto hizi ni moja tu. Nao wale ng'ombe saba wenye kukonda vibaya waliotoka nyuma yao ndio miaka saba, nayo yale masuke saba matupu yaliyonyaushwa na upepo wenye joto ndio miaka saba ya njaa. Hili ndilo lile neno, nililomwambia Farao, ya kuwa Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya. Tazama! Inakuja miaka saba yenye shibe kubwa katika nchi nzima ya Misri. Baadaye itatokea miaka saba yenye njaa; ndipo, hiyo shibe yote itakaposahauliwa katika nchi ya Misri, nayo njaa itaimaliza nchi hii. Hiyo shibe haitajulikana kabisa katika nchi hii kwa ajili ya hiyo njaa itakayoifuata, kwani itakuwa nzito sana. Farao akiota mara mbili ndoto moja, ni kwamba: Shauri hili limekwisha kukatwa kwake Mungu, yeye Mungu atalifanya upesi. Sasa Farao na ajionee mtu mwenye akili na werevu wa kweli, amweke kuwa mkuu wa nchi ya Misri! Farao na ampe nguvu ya kuweka wasimamizi katika nchi hii, wawatoze watu wa Misri fungu la tano hiyo miaka saba ya shibe. Hivyo vyakula vyote na wavikusanye katika hiyo miaka saba mizuri ijayo, wazilimbike hizo ngano vyanjani mwa Farao, waziangalie vema kuwa akiba za kula wao waliomo mijini. Watu wa nchi hii na wawekewe hivyo vilaji, wapate kula, hiyo miaka saba ya njaa itakapoingia katika nchi ya Misri, watu wa nchi wasimalizike kwa njaa. Maneno haya yakawa mazuri machoni pake Farao napo machoni pao watumishi wake. Farao akawauliza watumishi wa: Je? Tutaona wapi mtu kama huyu mwenye roho ya Mungu? Kisha Farao akamwambia: Kuwa kuwa Mungu amekujulisha haya yote, basi, hakuna mwenye akili na werevu wa kweli kama wewe. Sasa wewe utakuwa mkuu wa nyumba yangu, nao watu wangu wote sharti wayafanye, kinywa chako kitakayowaambia; mimi tu nitakupita ukuu kwa kukikalia kiti cha ufalme. Farao akamwambia Yosefu tena: Tazama! Nimekupa ukuu wa nchi yote ya Misri nzima. Kisha Farao akaitoa pete yake kidoleni pake, akaitia katika kidole cha Yosefu, akamvika nguo nyeupe za bafta nzuri, akamtia mkufu wa dhahabu shingoni. Kisha akamtembeza katika gari lake la kifalme la pili, akatanguliza watu waliopiga mbiu kwamba: Pigeni magoti! Ndivyo, alivyomweka kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri. Kisha Farao akamwambia Yosefu: Kweli mimi ni Farao, lakini usipotaka wewe, mtu ye yote katika nchi yote ya Misri asiinue mkono wala mguu wake. Farao akamwita Yosefu Safenati-Panea (Mponya Wazima), akampa Asenati, binti Potifera, mtambikaji wa Oni, kuwa mkewe. Kisha Yosefu akatoka kwenda kuzitazama nchi zote za Misri. Hapo, Yosefu aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri, alikuwa mwenye miaka 30, napo Yosefu alipotoka kwake Farao akatembea katika nchi zote za Misri. Hiyo miaka saba ya shibe nchi ikapata neema nyingi sana, naye Yosefu akavikusanya vilaji vyote vya hiyo miaka saba, iliyoipata nchi ya Misri, akavilimbika mijini akiagiza, vilaji vyote vya mashamba ya kila mji yaliyouzunguka yawekwe vyanjani mwake. Hivyo Yosefu akalimbika ngano, zikawa nyingi sana kama mchanga wa ufukoni, hata akaacha kuzipima, kwani hazikupimika. Mwaka wa njaa ulipokuwa haujaingia bado, Yosefu akazaliwa wana wawili, aliowazaa Asenati, binti Potifera, mtambikaji wa oni. Mwanawe wa kwanza Yosefu akamwita jina lake Manase (Msahaulishaji) kwa kwamba: Mungu amenisahaulisha masumbuko yangu yote nao mlango wote wa baba yangu. Naye wa pili akamwita jina lake Efuraimu (Mazao Mawili) kwa kwamba: Mungu amenipa kuzaa katika nchi ya ukiwa wangu. Hiyo miaka saba ya shibe, iliyoipata nchi ya Misri, ilipomalizika, ndipo, ile miaka saba ya njaa ilipoanza kuingia, kama Yosefu alivyosema; ikawa njaa katika nchi zote, ni nchi ya Misri tu iliyokuwa na chakula. Watu wote wa Misri walipoona njaa wakamililia Farao, awape chakula; naye Farao akawaambia watu wote: Nendeni kwa Yosefu! Nayo atakayowaambia yafanyizeni! Njaa ilipokwisha kuipata nchi yote nzima, ndipo, Yosefu alipovifungua vyanja vyote vya ngano vilivyokuwa kwao, akawauzia Wamisri ngano, nayo njaa ikawa kali katika nchi ya Misri. Watu wa nchi zote wakaja Misri kununua chakula kwa Yosefu, kwani njaa hiyo ilikuwa kali katika nchi zote. Yakobo alipoona, ya kuwa Misri vyakula viko, Yakobo akawaambia wanawe: Mbona mnatazamiana? Akasema: Tazameni, nimesikia, ya kuwa Misri vyakula viko! Telemkeni kwenda huko, mtununulie ngano huko, tupate kupona, tusife! Basi, kaka zake Yosefu kumi wakatelemka kununua ngano kule Misri. Lakini Benyamini, nduguye Yosefu, Yakobo hakumtuma kwenda na kaka zake, kwani alisema: Labda ataona kibaya njiani. Wana wa Isiraeli wakaingia katikati yao wengine waliokwenda kununua ngano, kwani njaa ilikuwa imeingia hata katika nchi ya Kanaani. Naye Yosefu alikuwa mtawala nchi hiyo, naye ndiye aliyewauzia ngano watu wote wa nchi hiyo. Kaka zake Yosefu walipofika kwake wakamwinamia, mpaka nyuso zao zikifika chini. Yosefu alipowaona kaka zake akawatambua, lakini akajitendekeza, kama hawajui, akasema nao maneno magumu, akawauliza: Mmetoka wapi? Wakasema: Tumetoka katika nchi ya Kanaani kuja huku kununua ngano. Ijapo Yosefu aliwatambua, wao hawakumtambua. Ndipo, Yosefu alipozikumbuka ndoto zake, alizoziota kwa ajili yao, kisha akawaambia: Mu wapelelezi, mmekuja kutazama, nchi hii inakokuwa wazi. Wakamwambia: Sivyo, bwana wetu. Watumwa wako wamkuja tu kununua ngano. Sisi sote tu wana wa mtu mmoja, sisi tu watu wa kweli; watumwa wako hawajawa bado wapelelezi. Lakini akawaambia: Sivyo, mmekuja kutazama, nchi hii inakokuwa wazi. Ndipo, waliposema: Sisi watumwa wako tulikuwa ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja katika nchi ya Kanaani; na sasa mdogo wetu yuko kwa baba yetu, lakini mmoja hayupo. Lakini Yosefu akwaambia: Ni hivyo, nilivyowaambia kwamba: Mu wapelelezi. Kwa neno hili nitawajaribu: Hivyo, Farao alivyo mzima, hamtatoka huku, ndugu yenu mdogo asipokuja huku. Toeni mmoja miongoni mwenu, aende kumchukua ndugu yenu! Nanyi wengine mtafungwa. Hivyo mtaumbuliwa, kama maneno yenu ni ya kweli, au kama sivyo; hivyo, Farao alivyo mzima, mu wapelelezi. Kisha akawafunga kifungoni siku tatu. Siku ya tatu Yosefu akawaambia: Fanyeni hivi, mpate kupona! Kwani mimi ni mtu mwenye kumcha Mungu. Kama ninyi m watu wa kweli, mwenzenu mmoja tu afungwe kifungoni! Lakini ninyi wengine nendeni kupeleka ngano za kuondoa njaa nyumbani mwenu! Kisha sharti mniletee ndugu yenu mdogo, maneno yenu yajulike kuwa ya kweli, msife. Wakafanya hivyo. Ndipo, waliposemezana wao kwa wao: Kweli hapa tunalipishwa tuliyomkosea ndugu yetu. Tulipoona, roho yake ilivyosongeka, naye alipotulalamikia, hatukumsikia. Kwa sababu hii hangaiko hili limetupata. Rubeni akawajibu kwamba: Sikuwaambia ninyi kwamba: Msimkosee mtoto? Lakini mlikataa kunisikia; sasa mnaona, damu yake inalipizwa. Nao hawakujua, ya kuwa Yosefu amewasikia, kwa kuwa walikuwa wanaye mkalimani. Ndipo, Yosefu alipoondoka kwenda kulia machozi. Aliporudi kusema nao, akamchukua Simeoni, akamfunga machoni pao. Kisha Yosefu akaagiza watu, wavijaze vyombo vyao ngano, nazo fedha zao za kila mmoja wazirudishe katika gunia lake, wawape hata pamba za njiani; nao wale wakawafanyizia hivyo. Kisha wakawachukuza punda wao mizigo yao ya ngano, wakatoka huko kwenda zao. Walipofika kambini, mmoja wao akalifungua gunia lake, ampe punda chakula, akaziona fedha zake hapo juu ndani ya gunia lake. Akawaambia ndugu zake: Kumbe fedha zangu zimerudishwa, zimo ndani ya gunia langu! Ndipo, mioyo yao ilipopigwa bumbuazi kwa kustuka, wakaambiana wao kwa wao: Mbona Mungu anatufanyizia haya? Waliporudi kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani wakamsimulia yote yaliyowapata njiani, wakasema: Yule bwana wa nchi hiyo ametuambia maneno magumu, akatusingizia kuwa watu wa kuipeleleza nchi hiyo, tukamwambia: Sisi tu watu wa kweli, hatujawa bado wapelelezi; sote tulikuwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu mmoja, naye mdogo sana yuko kwa baba yetu katika nchi ya Kanaani. Ndipo, yule bwana wa nchi hiyo alipotuambia: Hivi nitajua, ya kuwa m wakweli: mwenzenu mmoja mwacheni huku kwangu! Kisha chukueni vilaji vya kuondoa njaa nyumbani mwenu, mwende zenu! Kisha sharti mniletee ndugu yenu mdogo, nipate kujua, ya kuwa hamu wapelelezi, ya kuwa mu wakweli; ndipo, nitakapowapa naye ndugu yenu, nanyi mtaweza kuchuuza katika nchi hii. Ikawa walipoyamimina magunia yao wakaona kila mtu kifuko chake cha fedha katika gunia lake; walipoona, ya kuwa ni vifuko vya fedha zao kweli, wakashikwa na woga wote, wao na baba yao. Ndipo, baba yao Yakobo alipowaambia: Mwaninyang'anya wana wangu wote. Yosefu hayupo, Simeoni hayupo, sasa mnataka kumchukua Benyamini naye. Haya yote yamenipata! lakini Rubeni akamwambia baba yake: Wanangu wawili utawaua, nisipomrudisha Benyamini kwako. Mtie mkononi mwangu! Mimi nitamrudisha kwako. Lakini akasema: Huyu mwanangu hatatelemka pamoja nanyi, kwani kaka yake amekufa, naye amesalia peke yake; atakapopatwa na kibaya cho chote njiani katika hiyo safari mtakayokwenda mtanisukuma mimi mwenye mvi kushuka kuzimuni na kusikitika. Njaa ikawa nzito katika nchi. Walipokwisha kuzila hizo ngano, walizozileta toka Misri, baba yao akawaambia: Rudini huko kutununulia vilaji vichache! Ndipo, Yuda alipomwambia kwamba: Yule mtu alitushuhudia kwa ukali kwamba: Hamtauona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa nanyi. Ukitaka kumtuma huyu ndugu yetu kwenda pamoja na sisi, tutatelemka kukununulia vilaji; lakini usipotaka kumtuma, hatuwezi kutelemka, kwani yule mtu alituambia: Hamtauona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa nanyi. Ndipo, Isiraeli aliposema: Kwa nini mmenifanyizia haya mabaya ya kumpasha yule mtu habari, ya kuwa yuko ndugu yenu mwingine? Wakajibu: Yule mtu alituuliza mara kwa mara habari za kwetu na za udugu wetu kwamba: Baba yenu yuko mzima bado? Mna ndugu mwingine? Nasi hatukuwa na budi kumjibu hayo maulizo yake; tungalijuaje, ya kuwa anataka kutuambia: Sharti mmtelemshe ndugu yenu? Naye Yuda akamwambia baba yake Isiraeli: Mtume huyu kijana kwenda na mimi, tupate kuondoka kwenda huko, tupone, tusife sisi na wewe na watoto wetu. Mimi na niwe mdhamini wake, na umtafute mkononi mwangu! Nisipomrudisha na kumsimamisha mbele yako nitakuwa nimekukosea siku zote. Kama hatungalikawilia, tungalikuwa tumekwisha kurudi hata mara mbili. Basi, baba yao Isiraeli akawaitikia kwamba: Kama hayana budi kuwa hivyo, haya! Yafanyizeni! Chukueni vyomboni mwenu mazao ya nchi hii yanayosifiwa, tena mpelekeeni yule mtu kuwa matunzo yake: mafuta ya mkwaju machache na asali kidogo na manukato na uvumba na kungu na lozi! Tena chukueni mikononi mwenu fedha za mara mbili, nazo fedha zile zilizorudishwa katika magunia yenu sharti mzirudishe mikononi mwenu, labda yuko aliyekosa kwa kupotelewa na amri. Kisha mchukueni naye ndugu yenu, mwondoke kurudi kwake yule mtu! Naye Mwenyezi Mungu na awapatie kuhurumiwa usoni pake yule mtu, awafungulie ndugu yenu mwingine, mje naye hata naye Benyamini! Lakini mimi, kama nilivyopotelewa na wana, kama inanipasa, na nipotelewe tena na wana. Kisha hao watu wakayachukua hayo matunzo, nazo fedha za mara mbili wakazichukua mikononi mwao, naye Benyamini, wakaondoka kutelemka kwenda Misri. Walipomtokea Yosefu, naye Yosefu alipomwona Benyamini kuwa nao, akamwambia mkuu wa nyumba yake: Waingize watu hawa humo nyumbani! Kisha chinja nyama, uiandalie vizuri, kwani watu hawa watakula kwangu saa sita. Yule mtu akafanya, kama Yosefu alivyomwagiza, akawaingiza hao watu nyumbani mwa Yosefu. Lakini watu hao wakashikwa na woga kwa kuingizwa nyumbani mwake Yosefu, wakasema: Tumeingizwa humu kwa ajili ya hizo fedha zilizorudishwa hapo kwanza katika magunia yetu, apate kutusingizia na kutulipisha yaliyotuangukia, atuchukue sisi pamoja na punda wetu, tuwe watumwa wake. Kwa hiyo wakamkaribia yule mkuu wa nyumba ya Yosefu, wakasema naye hapo pa kuingia nyumbani, wakamwambia: E bwana, tulipotelemka safari ya kwanza kununua ngano, nasi tulipofika kambini, tukafungua magunia yetu, tukaona kila mtu fedha zake juu ndani ya gunia lake, nazo hizo fedha zetu zilikuwa zenye kipimo chao sawasawa, kwa hiyo tumezirudisha mikononi mwetu; nazo fedha nyingine tumetelemka nazo mikononi mwetu za kununua vilaji; hatumjui aliyeziweka hizo fedha zetu katika magunia yetu. Naye akasema: Tulieni tu, msiogope! Mungu wenu na Mungu wa baba yenu aliwapatia kilimbiko katika magunia yenu, fedha zenu zilifika kwangu. Kisha akamfungua Simeoni, akamleta kwao, akawaingiza nyumbani mwake Yosefu, akawapa maji ya kuiosha miguu yao, nao punda wao akawapata chakula. Nao wakayatengeneza matunzo yao, mpaka Yosefu akaja saa sita, kwani walisikia, ya kuwa watakula chakula huko. Yosefu alipoingia humo nyumbani, wakampelekea hayo matunzo mikononi mwao nyumbani mwake na kumwangukia hapo chini. Akawaamkia kwa upole, akawauliza: Baba yenu mzee, ambaye mliniambia, ya kuwa yuko mzima, na sasa hajambo? Wakamwambia: Mtumwa wako baba yetu hajambo, yuko mzima bado; kisha wakamwinamia na kumwangukia. Alipoyainua macho yake akamwona ndugu yake Benyamini aliyezaliwa na mama yake, akauliza: Kumbe huyu ni ndugu yenu mdogo, ambaye mliniambia habari zake? Akasema: Mungu na akugawie mema, mwanangu! Kisha Yosefu akakimbilia chumba kingine, apate kulia machozi, kwani alichafukwa na moyo kwa kumfurahia nduguye, namo mle chumbani machozi yakamtoka kweli. Alipokwisha kuunawa uso wake, akawatokea tena na kutulia kwa kujizuia, akaagiza: Leteni chakula! Wakamwandalia yeye peke yake nao ndugu zake peke yao nao Wamisri waliokula naye peke yao, kwani ni mwiko wa Wamisri kula chakula pamoja na Waebureo, huwachukiza. Wakawakalisha mbele yake, kama walivyofuatana: aliyezaliwa wa kwanza hapo palipoupasa ukubwa wake, naye mdogo hapo palipoupasa ujana wake; kwa hiyo hao watu wakastaajabu na kutazamana wao kwa wao. Wakawapa vyakula vilivyotoka mezani pake Yosefu, lakini Benyamini akaandaliwa vyakula vilivyovipita vyao wote kwa wingi mara tano. Kisha wakanywa, hata wakachangamshwa pamoja naye. Yosefu akamwagiza mkuu wa nyumba yake kwamba: Magunia ya watu hawa yajaze vilaji, kama wanavyoweza kuchukua, nazo fedha za kila mtu ziweke juu ndani ya gunia lake! Namo juu ndani ya gunia lake mdogo tia pamoja na fedha zake za ngano kikombe changu, hicho kikombe cha fedha. Akafanya hivyo, kama Yosefu alivyomwagiza. Asubuhi kulipopambazuka, wakapewa ruhusa kwenda zao, wao na punda wao. Walipokwisha kutoka mjini na kwenda mbali kidogo, ndipo, Yosefu alipomwambia mkuu wa nyumba yake: Ondoka, uwafuate hao watu na kupiga mbio! Utakapowapata waambie: Mbona hayo mema mliyofanyiziwa mnayalipa na kufanya mabaya? Kumbe hicho kikombe sicho, bwana wangu alichokinywea? Tena hukitumia cha kuagulia. Haya mliyoyafanya ni mabaya. Alipowapata akawaambia maneno yayo hayo. Wakamwambia: Kwa nini bwana wetu anasema maneno kama hayo? Yasiwajie watuma wako maneno kama hayo, wayafanye! Tazama! Hizo fedha, tulizoziona juu ndani ya magunia, tumezirudisha kwako toka nchi ya Kanaani. Tutawezaje kuiba fedha au dhahabu nyumbani mwa bwana wako? Atakayeonekana kuwa nacho miongoni mwao watumwa wako na afe! Nasi tutakaopona tutakuwa watumwa wake bwana wetu. Akaitikia kwamba: Basi, na viwe hivyo, kama mlivyosema! Atakayeonekana kuwa nacho, atakuwa mtumwa wangu, nanyi wengine mtakuwa hamna kosa. Wakashusha upesi chini kila mtu gunia lake, wakafungua kila mtu gunia lake. Naye yule mtu alipotafuta akaanza kwake mkubwa, akamaliza kwake mdogo; ndipo, kikombe kilipooneka katika gunia la Benyamini. Ndipo, wote walipozirarua nguo zao, wakawachukuza tena kila mtu punda wake mzigo ake, wakarudi mjini. Yuda na ndugu zake walipoingia nyumbani mwa Yosefu, naye alikuwa angalimo bado, nao wakamwangukia chini. Yosefu akawaambia: Ni tendo gani hilo, mlilolitenda? Hamjui, ya kuwa mtu kama mimi huangua? Yuda akajibu: Tumwambie nini bwana wetu? Tusemeje? Tutawezaje kujikania? Mngu anayaumbua maovu, watumwa wako waliyoyafanya; tazama, sisi pamoja naye aliyeonekana kuwa nacho hicho kikombe mkononi mwake tu watumwa wako. Naye akasema: Hili lisinijie, nifanye tendo kama hilo! Yule mtu aliyeoneka kuwa nacho hicho kikombe mkononi mwake yeye tu atakuwa mtumwa wangu, nanyi wengine nendeni na kutengemana kwa baba yenu! Ndipo, Yuda alipomkaribia na kumwambia: Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno masikioni pake bwana wangu! Makali yako yasimwakie mtumwa wako! Kwani wewe unalingana na Farao. Bwana wangu alipowauliza watumwa wake kwamba: Mna baba au ndugu? tukamwambia bwana wangu: Tuna baba, naye ni mzee, naye mtoto wa uzee wake yuko, lakini ndugu yake amekufa, akaachwa yeye peke yake wa mama yake, kwa hiyo baba yake anampenda. Ukawaambia watumwa wako: Sharti mmtelemshe, afike kwangu, nipate kumwona kwa macho yangu. Nasi tukamwambia bwana wangu: Huyu kijana hataweza kumwacha baba yake; akimwacha baba yake, huyo atakufa. Ukawaambia watumwa wako: Ndugu yenu mdogo asipotelemka pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena. Tulipopanda kwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamsimulia hayo maneno ya bwana kidogo! Kisha baba yetu alipotuambia: Rudini kutununulia vilaji wangu! Tukasema: Hatuwezi kutelemka; lakini ndugu yetu mdogo akienda pamoja nasi, tutatelemka; kwani hatuwezi kuuona uso wake yule mtu, ndugu yetu mdogo asipokuwa nasi. Ndipo, mtumwa wako baba yangu alipotuambia: Ninyi mnajua, ya kuwa mke wangu alinizalia wana wawili; mmoja alipoondoka kwangu, nikasema: Ameraruliwa na nyama, maana sikumwona tena mpaka sasa. Sasa mkimchukua huyu naye na kumtoa kwangu, akipatwwa na kibaya njiani, mtanisukuma mimi mwenye mvi kushuka kuzimuni kwa kuyaona hayo mabaya. Kama ningefika kwa mtumwa wako, baba yangu, tusipokuwa naye huyu kijana, ambaye roho ya baba ilifungamana nayo roho yake, baba akaona, ya kuwa hayuko, angekufa papo hapo, nasi watumwa wako tungekuwa tunamsukuma mtumwa wako, baba yetu, mwenye mvi kushuka kuzimuni na kusikitika. Kwani mimi, mtumwa wako, nimejitoa kwa baba kuwa mdhamini wake huyu kijana, nikamwambia: Nisipomrudisha kwako, nitakuwa nimemkosea baba yangu siku zote. Sasa mtumwa wako na akae mahali pake huyu kijana kuwa mtumwa wa bwana wangu, naye huyu kijana na apande na kaka zake kwenda kwao! Kwani nitawezaje kupanda kwenda kwa baba yangu, huyu kijana asipokuwa pamoja na mimi? Sitaweza kuyaona hayo mabaya yatakayompata baba yangu. Yosefu asipoweza kuvumilia tena kwa ajili yao wote waliosimama kwake, ndipo alipoita kwamba: Watoeni wote humu mwangu! Kwa hiyo hakusimama mtu mwake, Yosefu alipojitambulisha kwa ndugu zake. Lakini alipopaza sauti kwa kulia, Wamisri wakavisikia, nao wa nyumbani mwa Farao wakavisikia. Kisha Yosefu akawaambia ndugu zake: Ni mimi Yosefu! Baba yangu yuko mzima bado? Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwani walimstukia. Ndipo, Yosefu alipowaambia ndugu zake: Nifikieni karibu! Nao walipokwisha kumkaribia, akawaambia: Ni mimi ndugu yenu Yosefu, mliyemwuza kupelekwa Misri. Lakini sasa msisikitike, wala msijikasirikie, ya kuwa mliniuza kupelekwa huku! Kwani Mungu ndiye aliyenituma kwenda mbele yenu, nipate kuwaponya. Kwani huu ni mwaka wa pili wa kuingia njaa katika nchi hii, ingaliko miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna. Kwa hiyo Mungu alinituma kwenda mbele yenu, niwapatie ninyi masao katika nchi hii na wokovu mkubwa wa kuwaponya ninyi. Sasa sio ninyi mlionituma kuja huku, ila ni Mungu mwenyewe. Naye akaniweka kuwa baba yake Farao na bwana wa nyumba yake yote na mtawala nchi zote za Misri. Pigeni mbio, mpande kwenda kwa baba yangu, mmwambie: Hivi ndivyo, anavyosema mwanao Yosefu: Mungu ameniweka kuwa bwana wa nchi yote nzima ya Misri; telemka kuja kwangu, usikawilie! Na ukae katika nchi ya Goseni, upate kuwa karibu yangu, wewe na wanao na wana wa wanao na mbuzi na kondoo wako na ng'ombe wako navyo vyote, ulivyo navyo. Nitakutunza huku, kwani ingaliko bado miaka mitano ya njaa; zisiangamizwe mali zako wewe nazo zao walio wa mlango wako, nazo zao wote, ulio nao. Macho yenu ninyi yanaona, nayo macho ya ndugu yangu Benyamini yanaona, ya kuwa ni kinywa changu mimi kinachosema nanyi. Msimulieni baba yangu, utukufu wangu wote ulivyo huku Misri, nayo yote, mliyoyaona! Pigeni mbio, mmtelemshe baba yangu kuja huku! Kisha akamkumbatia nduguye Benyamini, akali machozi; Benyamini naye akalia machozi shingoni pake. Nao kaka zake wote akanoneana nao pamoja na kulia machozi; kisha kaka zake wakaongea naye. Uvumi uliposikilika nyumbani mwa Farao kwamba: Ndugu zake Yosefu wamefika! akapendezwa Farao nao watumishi wake. Naye Farao akamwambia Yosefu: Waaambie ndugu zako: Fanyeni hivi: wachukuzeni nyama wenu mizigo, mpate kwenda zenu! Mtakapofika katika nchi ya Kanaani, mchukueni baba yenu nao wa milango yenu, mje kwangu! Nitwapa kipande cha nchi ya Misri kilicho kizuri, mle manono ya nchi hii! Wewe umekwisha kuagizwa, uwaambie: Fanyeni hivi: jichukulieni huku katika nchi ya Misri magari ya kuwachukulia watoto wenu na wake zenu! Naye baba yenu mchukueni, mje naye! Msijiumize kwa ajili ya vyombo vyenu! Kwani mema yote ya nchi nzima ya Misri ni yenu! Nao wana wa Isiraeli wakafanya hivyo, maana Yosefu akawapa magari kwa ile amri ya Farao, akawapa nazo pamba za njiani. Nao wote akawapa nguo za zikukuu, kila mmoja yake; lakini Benyamini akampa fedha 300 na nguo tano za sikukuu. Naye baba yake akampelekea vitu hivi: punda kumi waliochukua vitu vizuri vya Misri na majike ya punda kumi waliochukua ngano na chakula kingine na pamba za njiani za baba yake. Alipoagana na ndugu zake, waende zao, akawaambia: Msigombane njiani! Ndivyo, walivyotoka Misri, wapande kwenda katika nchi ya Kanaani kwa baba yao Yakobo. Wakamsimulia kwamba: Yosefu yuko mzima bado, naye ndiye anayeitawala nchi yote nzima ya Misri; lakini moyo wake ukapigwa bumbuazi, hakuyategemea maneno yao. Wakamwambia maneno yote, Yosefu aliyowaambia; naye alipoyaona hayo magari, Yosefu aliyoyatuma kumchukua, ndipo, roho yake ilipomrudia baba yao Yakobo. Kisha Isiraeli akasema: Lililo kuu ni hili: mwanangu Yosefu angaliko mzima. Nitakwenda, nimwone, kabla sijafa. Isiraeli akaondoka pamoja nayo yote, aliyokuwa nayo, akaja Beri-Seba; ndiko, alikomchinjia Mungu wa baba yake Isaka ng'ombe za tambiko. Naye Mungu akamtokea Isiraeli usiku, akamwita kwamba: Yakobo! Yakobo! Akaitikia: Mimi hapa! Naye akamwambia: Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako; usiogope kutelemka Misri! Kwani ndiko, nitakakokupa kuwa taifa kubwa. Mimi nitatelemka pamoja na wewe kwenda Misri, nami nitakupandisha tena kuja huku, naye Yosefu atayafumba macho yako kwa mkono wake. Yakobo alipoondoka Beri-Seba, wana wa Isiraeli wakampandisha baba yao Yakobo garini nao watoto wao na wake zao, ndiyo yale magari, Farao aliyoyatuma kumchukua. Wakayachukua nayo makundi yao na mapato yao, waliyoyapata katika nchi ya Kanaani, wakafika Misri, yeye Yakobo nao wa uzao wake wote pamoja naye. Wanawe na wajukuu wake nao wanawe wa kike na wajukuu wake wa kike nao wa uzao wake wote aliwapeleka Misri kwenda naye. Haya ndiyo majina ya wana wa Isiraeli waliokwenda Misri. Yakobo na wanawe: Mwana wa kwanza wa Yakobo ni Rubeni. Nao wana wa Rubeni ni Henoki na Palu na Hesironi na Karmi. Nao wana wa Simeoni ni Yemueli na Yamini na Ohadi na Yakini na sohari na Sauli, mwana wa mwanamke wa Kanaani. Nao wana wa Lawi ni Gersoni na Kehati na Merari. Nao wana wa Yuda ni Eri na Onani na Sela na Peresi na Zera; lakini Eri na Onani walikuwa wamekufa katika nchi ya Kanaani. Nao wana wa peresi walikuwa Hesironi na Hamuli. Nao wana wa Isakari ni Tola na Puwa na Yobu na Simuroni. Nao wana wa Zebuluni ni Seredi na Eloni na Yaleli. Hawa ndio wana wa Lea, aliomzalia Yakobo huko Mesopotamia, naye mwanawe wa kike ni Dina. Wanawe wote pamoja, wa kiume na wa kike, ni watu 33. Nao wana wa Gadi ni Sifioni na Hagi na suni na Esiboni, tena Eri na Arodi na Areli. Nao wana wa Aseri ni Imuna na Isiwa na Iswi na Beria na umbu lao Sera; nao wana wa Beria ni Heberi na Malkieli. Hawa ndio wana wa Zilpa, Labani aliyempa mwanawe Lea; naye alimzalia Yakobo hawa watu 16. Wana wa Raheli, mkewe Yakobo, ni Yosefu na Benyamini Naye Yosefu katika nchi ya Misri alizaliwa Manase na Efuraimu; ndio, aliomzalia Asenati, binti Potifera, mtambikaji wa Oni. Nao wana wa Benyamini ni Bela na Bekeri na Asibeli, Gera na Namani, Ehi na Rosi, Mupimu na Hupimu na Ardi. Hawa ndio wana wa Raheli, Yakobo aliozaliwa; wote pamoja ni watu 14. Nao wana wa Dani ni Husimu. Nao wana wa Nafutali ni Yaseli na Guni na Yeseri na Silemu. Hawa ndio wana wa Biliha, Labani aliyempa mwanawe Raheli; naye alimzalia Yakobo hawa watu 7. Watu wote waliokwenda Misri na Yakobo ni 66; ndio waliotoka kiunoni mwake, tena wake zao wana wa Yakobo. Nao wana wa Yosefu aliozaliwa huko Misri, ni watu wawili; hivyo watu wote pia wa mlango wa Yakobo waliokuja Misri walikuwa 70. Yakobo akamtuma Yuda kwenda mbele yake kwa Yosefu, amwonyeshe nchi ya Goseni, kisha wakaiingia hiyo nchi ya Goseni. Ndipo, Yosefu alipolitandika gari lake, akamwendea baba yake Isiraeli huko Goseni. Alipomwonekea, akamkumbatia shingoni akalia machozi hapo shingoni pake kitambo kizima. Kisha Isiraeli akamwambia Yosefu: Sasa na nife, kwani nimekwisha kuuona uso wako, ya kuwa u mzima bado. Kisha Yosefu akawaambia ndugu zake nao wa mlango wa baba yake: Nitapanda kumpasha Farao habari ya kwamba: Ndugu zangu nao wa mlango wa baba yangu waliokaa katika nchi ya Kanaani wamefika kwangu. Nao watu hawa ni wachungaji, kwani ni wenye makundi, nao mbuzi na kondoo wao na ng'ombe wao nayo yote, waliyokuwa nayo, wameyaleta huku. Naye Farao atakapowaita na kuwauliza: Kazi yenu nini? na mmwambie: Watumwa wako ni wachungaji tangu ujana wetu mpaka sasa; nasi tulivyo, ndivyo, nao baba zetu walivyokuwa, kusudi mpate kukaa katika nchi ya Goseni; kwani Wamisri huwachukiza wachungaji wote. Kisha Yosefu akaingia kwake Farao, akampasha habari kwamba: Baba yangu na ndugu zangu na mbuzi na kondoo wao na ng'ombe wao pamoja nayo yote, waliyokuwa nayo, wametoka katika nchi ya Kanaani, sasa wako katika nchi ya Goseni. Alikuwa amewachukua ndugu zake watano waliozaliwa wa mwisho kuwasimamisha mbele ya Farao. Farao alipowauliza: Kazi yenu nini? wakamwambia Farao: Watumwa wako ni wachungaji; nasi tulivyo, ndivyo, nao baba zetu walivyokuwa. Tena wakamwambia Farao: Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwani mbuzi na kondoo wao watumwa wako hawana malisho, kwani njaa ni nzito katika nchi ya Kanaani; sasa acha, watumwa wako wakae katika nchi ya Goseni! Ndipo, Farao alipomwambia Yosefu kwamba: Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako. Basi, nchi ya Misri iko wazi machoi pako; mkalishe baba yako pamoja na ndugu zako katika nchi iliyo nzuri zaidi! Na wakae katika nchi ya Goseni! Nao, uwajuao kuwa mafundi wa kazi hiyo, uwaweke kuwa wakuu wao wanaoyachunga makundi yangu. Kisha Yosefu akampeleka baba yake Yakobo, akamsimamisha mbele ya Farao, naye Yakobo akambariki Farao. Farao alimpomwuliza Yakobo: Miaka yako ya kuwapo ni mingapi? Yakobo akamjibu Farao: Siku za miaka ya kukaa huku ugenini ni miaka 130. Siku za miaka ya maisha yangu ni chache, tena ni mbaya, hazikufika kuwa nyingi kama siku za miaka ya kuwapo za baba zangu, walizozikaa huku ugenini. Yakobo akambariki Farao, kisha akatoka mwake Farao. Yosefu akampatia baba yake na ndugu zake mahali pa kukaa, akawapa kipande cha nchi ya Misri, wakichukue, nacho kilikuwa nchi nzuri zaidi katika nchi ya Ramusesi, kama Farao alivyoagiza. Yosefu akamtunza baba yake na ndugu zake nao wote wa mlango wa baba yake akiwapa chakula kwa hesabu ya watoto wao. Chakula hakikuwako katika nchi zote, kwa kuwa njaa ilikuwa nzito sana, nayo nchi ya Misri nayo nchi ya Kanaani zikaenda kuzimia kwa ajili ya njaa. Yosefu akazikusanya fedha zote zilizopatikana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani kwa kuuza ngano, watu walizozinunua; naye Yosefu akazipeleka hizo fedha nyumbani mwake Farao. Fedha zilipotoweka katika nchi ya Misri, Wamisri wote wakaja kwa Yosefu, wakamwambia: Tupe chakula! Mbona tufe machoni pako, kwa kuwa hatuna fedha? Naye Yosefu akasema: Leteni nyama, kama hamna fedha! Ndipo, walipopeleka kwa Yosefu nyama, waliowafuga, naye Yosefu akawapa chakula kwa farasi wao na kwa makundi yao ya mbuzi na kondoo na kwa makundi yao ya ng'ombe na kwa punda wao; ndivyo, alivyowatunza mwaka huo na kuwapa chakula kwa makundi yao yote. Mwaka huo ulipokwisha, wakaja kwake nao mwaka wa pili, wakamwambia: Hatutaki kumficha bwana wetu, ya kama fedha zimekwisha, nayo makundi ya nyama, tuliowafuga, wamekwenda kwa bwana wetu, hakuna yetu tena yaliyosalia mbele ya bwana wetu, isipokuwa miili yetu na mashamba yetu. Mbona tufe machoni pako sisi na mashamba yetu? Tununue sisi na mashamba yetu kwa chakula, sisi na mashamba yetu tuwe mali zake Farao! Tena tupe mbegu, tusife, nayo mashamba yasiwe mapori matupu! Ndivyo, Yosefu alivyomnunulia Farao mashamba yote ya Misri, kwani Wamisri waliuza kila mtu shamba lake, kwani njaa ilikuwa kali kwao; ndivyo, hiyo nchi ilivyopata kuwa yake Farao mwenyewe. Nao watu akawahamisha kukaa mijini toka mpaka wa kwanza wa Misri hata mpaka wake wa mwisho. Mashamba ya watambikaji tu hakuyanunua, kwani hao watambikaji walikatiwa hayo mashamba na Farao kuwa chakula chao, nao wakajitunza na kuitumia hiyo haki, Farao aliyowapa; kwa sababu hii hawakuyauza mashamba yao. Kisha Yosefu akawaambia watu: Tazameni, nimewanunua leo ninyi na mashamba yenu kuwa mali zake Farao; ninawapa hapa mbegu za kupanda katika mashamba yenu. Hapo, mtakapovuna, sharti mmpe Farao fungu la tano! Mafungu manne yatakuwa yenu ya kupanda mashambani na ya kula ninyi nao waliomo manyumbani mwenu na watoto wenu. Ndipo, waliposema: Umetuponya. Tumeona mapendeleo machoni pa bwana wetu, na tuwe watumwa wake Farao! Hayo maongozi, Yosefu aliyoyaweka, yako mpaka siku hii ya leo kwamba: Fungu la tano la mapato ya mashamba ya Misri ni lake Farao. Mashamba yasiyouzwa kuwa yake Farao ni yale ya watambikaji peke yao tu. Ndivyo, Waisiraeli walivyokaa huko Misri katika nchi ya Goseni, wakaichukua kuwa yao, wakazaa wana, wakawa wengi sana. Yakobo akawapo katika nchi ya Misri miaka 17; hivyo siku za miaka ya maisha yake Yakobo zikawa miaka 147. Siku za kufa kwake Isiraeli zilipofika karibu, akamwita mwanawe Yosefu, akamwambia: Kama nimeona upendeleo machoni pako, uweke mkono wako chini ya kiuno changu, unifanyizie wema na welekevu huu, usinizike huku Misri, nipate kulala kwa baba zangu. Kwa hiyo unichukue na kunitoa huku Misri, upate kunizika kaburini mwao! Naye akasema: Nitafanya, kama ulivyosema. Aliposema: Uniapie! akamwapia. Kisha Isiraeli akauinamia upande wa kichwani wa kitanda na kusali. Ikawa, mambo hayo yalipokwisha, wakamwambia Yosefu: Tazama! Baba yako ni mgonjwa. Ndipo, alipowachukua wanawe wawili Manase na Efuraimu kwenda naye. Walipompasha Yakobo habari kwamba: Tazama! Mwanao Yosefu anakuja kwako, Isiraeli akajitia nguvu, apate kukaa kitandani. Yakobo akamwambia Yosefu: Mwenyezi Mungu alinitokea Luzi katika nchi ya Kanaani, akanibariki, akaniambia: Utaniona, nikikupa kuzaa wana, nikupe kuwa wengi, uwe mkutano wa makabila ya watu; kisha nchi hii nitawapa wao wa uzao wako wajao nyuma yako, mwichukue kuwa yenu kale na kale. Sasa wanao wawili uliowazaa katika nchi hii ya Misri, nilipokuwa sijafika huku Misri, ni wangu; Efuraimu na Manase watakuwa wangu, kama Rubeni na Simeoni walivyo wangu, nao wanao wengine, utakaowazaa nyuma yao, watakuwa wako; lakini wale wataitwa pamoja na majina ya ndugu zao, wagawiwe nao mafungu yao ya nchi yatakayokuwa yao. Nami nilipotoka Mesopotamia nilifiwa na Raheli njiani katika nchi ya Kanaani, uliposalia mwendo wa kipande kifupi tu kufika Efurata, nami nikamzika huko kwenye njia ya kwenda Efurata, ndio Beti-Lehemu. Isiraeli alipowaona wana wa Yosefu akauliza: Hawa ni nani? Yosefu akamwambia baba yake: Ndio wanangu, Mungu alionipa huku; ndipo, alipomwambia: Walete kwangu niwabariki! Maana macho yake Isiraeli yalikuwa yameguiwa na kiza, hayakuweza kuona kwa ajili ya uzee. Yosefu alipowafikisha karibu yake, akawanonea na kuwakumbatia. Kisha Isiraeli akamwambia Yosefu: Mimi sikuyawaza, ya kwamba nitauona uso wako, tena tazama! Mungu amenipa kuwaona nao wa uzao wako! Ndipo, Yosefu alipowaondoa magotini pake, akamwinamia na kuufikisha uso wake chini. Kisha Yosefu akawachukua wote wawili, Efuraimu kwa mkono wake wa kuume na kumweka kushotoni kwake Isiraeli, naye Manase kwa mkono wake wa kushoto na kumweka kuumeni kwake Isiraeli; ndivyo, alivyowapeleka kwake. Lakini Isiraeli akaupeleka mkono wake wa kuuume, akaubandika kichwani pake Efuraimu aliyekuwa mdogo, nao mkono wake wa kushoto akaubandika kichwani pake Manase, naye akavifanya kusudi akiwabandikia mikono hivyo, kwani Manase ndiye aliyezaliwa wa kwanza. Kisha akambariki Yosefu na kusema: Mungu, ambaye baba yangu Aburahamu na Isaka walifanya mwenendo machoni pake, yeye Mungu alikuwa mchungaji wangu tangu hapo, nilipozaliwa, mpaka siku hii ya leo; naye malaika aliyenikomboa katika mabaya yote na awabariki hawa vijana, jina langu nayo majina ya baba zangu Aburahamu na Isaka yatajwe kwao, wawe wengi sana katika nchi hii! Yosefu alipoona, ya kuwa baba yake ameubandika mkono wake wa kuume kichwani pake Efuraimu hakupendezwa; kwa hiyo akaushika huo mkono wa baba yake, auondoe kichwani pake Efuraimu, apate kuubandika kichwani pake Manase. Naye Yosefu akamwambia baba yake: Hivi sivyo, baba, kwani huyu ni wa kwanza; ubandike mkono wako wa kuume kichwani pake! Lakini baba yake akakataa akisema: Navijua, mwanangu, navijua kweli; huyu naye atakuwa kabila la watu, huyu naye atakuwa mkubwa, lakini ndugu yake mdogo atakuwa mkubwa kuliko yeye, nao wa uzao wake watakuwa mataifa mengi. Kisha akawabariki siku hiyo kwamba: Mwisiraeli atakapobariki atalitaja jina lako kwamba: Mungu na akupe kuwa kama Efuraimu na kama Manase! Hapa napo akamtaja Efuraimu mbele ya Manase. Kisha Isiraeli akamwambia Yosefu: Tazama! Mimi ninakufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, awarudishe katika nchi ya baba zenu. Nami nimekupa fungu moja zaidi ya ndugu zako, nililolichukua kwao Waamori kwa upanga wangu na kwa upindi wangu. Kisha Yakobo akawaita wanawe, akawaambia: Kusanyikeni, niwaeleze, yatakayowapata siku za sasa zitakapokwisha! Kusanyikeni, wana wa Yakobo, msikilize! Msikilizeni baba yenu Isiraeli! Wewe Rubeni, u mwana wa kwanza, u nguvu yangu na uwezo wangu wa kwanza, ukuu wako hutukuzwa, ukuu wako ni wa nguvu. Lakini kwa kububujika kama maji hutapata ukuu wa kweli, kwani ulipokipanda kitanda cha baba yako, ndipo, ulipoyachafua malalo yangu kwa kuyapandia. Simeoni na Lawi ni ndugu kweli, panga zao ni vyombo vya ukorofi. Roho yangu isiingie penye njama yao, wala moyo wangu usifanye bia na mikutano yao! Kwani kwa makali yao waliua watu, kwa majivuno yao wakakata madume ya ng'ombe mishipa. Na yaapizwe makali yao kwa kuwa yenye nguvu! Na yaapizwe machafuko yao kwa kuwa yenye upingani! Na niwagawanye kwao Wayakobo, na niwatawanye kwao Waisiraeli! Wewe Yuda, ndugu zako watakusifu; mkono wako utawakamata wachukivu wako penye kosi, nao wana wa baba yako watakuangukia. Yuda ni mwana simba. Mwanangu, ulipokwisha kukamata, hupanda kupumzika na kulala kama simba au kama mamake simba; yuko nani atakayekuamsha? Bakora ya kifalme haitaondoka kwake Yuda, wala fimbo la mwenye amri halitaondoka miguuni pake, mpaka atakapokuja mwenye kutuliza, ambaye makabila ya watu watamtii. Kipunda chake hukifunga mizabibuni, naye mwana punda humlisha miche ya mizabibu mizuri, huyafua mavazi yake katika mvinyo, nazo nguo zake katika damu za zabibu. Macho yake huwa mekundu kwa kunywa mvinyo, nayo meno yake huwa meupe kwa kunywa maziwa. Zebuluni atakaa pwani, Bahari Kubwa iliko, huko pwani, merikebu zinakofikia, apakane nao Wasidoni. Isakari ni punda mwenye mifupa migumu, hupenda kulala, katikati ya mazizi ya kondoo. Atakapoona matuo kuwa mema, atakapoiona nayo nchi hii kuwa ya kumpendeza, ndipo, atakapouinamisha mgongo wake kuchukua mizigo, awe mtumishi wa kufanya kazi za nguvu. Dani atawaamua walio watu wake akiwa kama wenzake walio mashina ya Isiraeli. Dani atakuwa nyoka njiani, atakuwa piri penye mikondo, awaume farasi visigino, waliowapanda waanguke nyuma. Ninaungojea wokovu wako, Bwana! Gadi atashambuliwa na vikosi vya vita, lakini naye atawashambulia na kuwanyatia. Kwake Aseri ndiko, vyakula vya manono vitakakotoka, naye ndiye atakayewapatia wafalme vyakula vya urembo. Nafutali ni kulungu aliyefunguliwa kukimbia, huimba nyimbo zilizo nzuri zaidi. Yosefu ni tawi la mti wa matunda, tawi la mti wa matunda ulioko kwenye mboji, kwa hiyo matawi yake hutambaa na kuufunika ukuta. Ijapo wapiga mishale wamchokoze kwa kumgombeza na kumchukia, upindi wake hushupaa vivyo hivyo, nazo nguvu za mikono yake ziko tayari vivyo hivyo, yumo mikoni mwake amtawalaye Yakobo, hushikwa na mchungaji aliye mwamba wa Isiraeli. Mungu wa baba yako ndiye atakayekusaidia Mwenyezi Mungu ndiye atakayekubariki kwa mbaraka zitokazo mbinguni juu na kwa mbaraka zitokazo vilindini ndani ya nchi na kwa mbaraka zitokazo maziwani na tumboni. Mbaraka za baba yako zina nguvu kuzishinda mbaraka zao walionizaa, zitakupendeza kuliko matunu ya vilima vya kale na kale. Hizo ndizo zitakazokijia kichwa chake Yosefu, nao utosi wake yeye aliyewekwa kwa kutengwa na ndugu zake. Benyamini ni mbwa wa mwitu mwenye uchu wa damu, asubuhi hula mawindo, jioni hugawanya mateka. Haya ndiyo mashina yote kumi na mawili ya Isiraeli, nayo haya ndiyo yote, baba yao aliyowaambia alipowabariki, naye aliwabariki na kumpa kila mmoja mbaraka yake yeye. Kisha akawaagiza na kuwaambia: Mimi sasa nitakapochukuliwa kwenda kwao walio ukoo wangu, sharti mnizike kwa baba zangu katika lile pango, lililoko shambani kwake Mhiti Efuroni! Ndilo pango lile lililoko shambani kwa Makipela kuelekea Mamure; shamba hilo Aburahamu alilinunua kwa Mhiti Efuroni kuwa mahali pake yeye pa kuzikia. Mle pangoni ndimo, walimomzika Aburahamu na mkewe Sara, naye Isaka na mkewe Rebeka waliwazika humo, naye Lea nilimzika humo. Ndilo lile shamba lililonunuliwa kwa wana wa Hiti pamoja na lile pango lililoko. Yakobo alipokwisha kuwaagiza wanawe maneno haya akaikunja miguu yake kitandani, akazimia, akachukuliwa kwenda kwao walio wa ukoo wake. Yosefu akamwangukia baba yake usoni, akamlilia na kumnonea. Kisha Yosefu akawaagiza watumishi wake waganga, wampake baba yake manukato; ndipo, hao waganga walipompaka Isiraeli manukato, mpaka siku 40 zikitimia, kwani kuzitimiza hizo siku ndio desturi ya kupaka manukato. Nao Wamisri akamwombolezea siku 70. Siku za maombolezo zilipokwisha pita, Yosefu akawaambia wao wa nyumbani mwake Farao kwamba: Kama nimeona upendeleo machoni penu, semeni masikioni pake Farao ya kwamba: Baba yangu ameniapisha kwamba: Tazama! Mimi ninakufa; sharti unizike katika kaburi langu, nililojichimbia katika nchi ya kanaani. Sasa ninataka kupanda kwenda huko, nimzike baba yangu, kisha nirudi. Naye Farao akasema: Panda kwenda huko, umzike baba yako, kama alivyokuapisha. Yosefu alipopanda kwenda huko kumzika baba yake, wakaenda naye watumwa wazee wote wa nyumbani mwake Farao nao wazee wote wa nchi ya Misri, nao wote wa mlango wa Yosefu nao ndugu zake nao wote wa mlango wa baba yake; watoto wao tu na mbuzi na kondoo na ng'ombe wao waliwaacha katika nchi ya Goseni. Nayo magari na wapanda farasi wakapanda naye, wakawa kikosi kikubwa sana. Walipofika pake Atadi pa kupuria ngano palipo ng'ambo ya huko ya Yordani wakafanya maombolezo makuu yenye vilio kabisa. Ndivyo, Yosefu alivyolala matanga siku saba kwa ajili ya baba yake. Wenyeji wa nchi ya Kanaani walipoyaona hayo matanga pake Atadi pa kupuria ngano wakasema: Matanga haya ya Wamisri ni makuu kweli, kwa sababu hii wakapaita jina lake mahali pale palipo ng'ambo ya huko ya Yordani: Tanga la Misri. Kisha wanawe wakayafanya yayo hayo, aliyowaagiza: wao wanawe wakamchkua na kumpeleka katika nchi ya Kanaani, kisha wakamzika katika lile pango katika shamba la Makipela, ndilo shamba lile, Aburahamu alilolinunua kwa Mhiti Efuroni kuwa mahali pake pa kuzikia, napo palikuwa panaelekea Mamure. Yosefu alipokwisha kumzika baba yake akarudi Misri, yeye na ndugu zake nao wote waliopanda naye kwenda kumzika baba yake. Lakini kaka zake Yosefu wakaogopa, kwa kuwa baba yao amekufa, wakasema mioyoni: Labda Yosefu atatuchukia, atulipize mabaya, tuliyomfanyizia. Kwa hiyo wakatuma kwake Yosefu kumwambia kwamba: Baba yako alipokuwa hajafa bado alituagiza kwamba: Hivi ndivyo, mtakavyomwambia Yosefu: E ndugu, yaondoe mapotovu na makosa yao ndugu zako! Kwani walikufanyizia mabaya. Sasa waondolee watumishi wa Mungu wa baba yako hayo mapotovu! Yosefu akalia machozi, walipomwambia maneno haya. Kisha kaka zake wenyewe wakaenda, wakamwangukia na kumwambia: Sisi hapa tu watumwa wako. Lakini Yosefu akawaambia: Msiogope! Je? Mimi ninapashika mahali pake Mungu? Kweli ninyi mwaliwaza kunifanyizia mabaya, lakini Mungu aliyageuza kuwa mema, ayafanye yaliyo waziwazi leo, aponye watu wengi. Kwa hiyo msiogope sasa! Mimi nitawatunza ninyi na watoto wenu. Hivyo akawatuliza mioyo akisema nao kwa upole. Yosefu akakaa Misri, yeye pamoja nao walio wa mlango wa baba yake; nayo miaka yake Yosefu ya kuwapo ilikuwa 110. Yosefu akaona wana wa Efuraimu hata kizazi cha tatu, nao wana wa Makiri, mwana wa Manase, wakazaliwa magotini pake Yosefu. Kisha Yosefu akawaambia ndugu zake: Mimi ninakufa, lakini ninyi Mungu atawapatia njia ya kuwatoa katika nchi hii na kuwapandisha kwenda katika hiyo nchi, aliyowaapia akina Aburahamu na Isaka na Yakobo kuwapa. Kisha Yosefu akawaapisha wana wa Isiraeli kwamba: Hapo, Mungu atakapowakagua ninyi, sharti mwichukue mifupa yangu kwenda nayo! Kisha Yosefu akafa mwenye miaka 110, wakampaka manukato, wakamweka ndani ya sanduku huko Misri. Haya ndiyo majina yao wana wa Isiraeli walioingia Misri; nao walikuja pamoja na Yakobo, kila mtu na mlango wake. Rubeni, Simeoni, Lawi na Yuda, Isakari, Zebuluni na Benyamini, Dani na Nafutali, Gadi na Aseri. Wao wote waliotoka viunoni mwa Yakobo walikuwa watu 70. Naye Yosefu alikuwa yuko kule Misri. Yosefu alipokwisha kufa na ndugu zake wote nacho hicho kizazi chote, wana wa Isiraeli wakazaa wana, wakazidi kuwa wengi na wenye nguvu sanasana, wakajieneza katika nchi hiyo. Kisha akaondokea mfalme mpya asiyemjua Yosefu. Naye akawaambia watu wake: Tazameni! Ukoo wa wana wa isiraeli unatushinda kwa wingi na kwa nguvu. Na tuwaendee kwa werevu, wasizidi kuwa wengi. Kwani itakuwa, vita vitakapotupata, watarudi upande wa adui zetu, wapigane nasi, wapate kuiteka nchi hii. Kwa hiyo wakawawekea wasimamizi wakali, wawatese na kuwafanyisha kazi ngumu, wakamjengea Farao miji ya kulimbikia vyo vyote, ndio Pitomu na Ramusesi. Lakini hivyo, walivyowatesa, ndivyo, walivyoendelea kuwa wengi na kuenea po pote, kwa hiyo wana wa Isiraeli wakawa kama tapisho kwao Wamisri, nao wakawafanyisha wana wa Isiraeli kazi za utumwa na kuwakorofisha. Wakawakalisha kuwa wenye uchungu siku zote kwa kuwafanyisha kazi ngumu za utumwa za kuumba na za kuchoma matofali na za kulima mashamba; hivyo wakawafanyisha kazi zo zote za utumwa za kuwatumikia, wakiwakorofisha. Kisha mfalme wa Misri akawaagiza wazalishaji wa Kiebureo, mmoja jina lake Sifura, wa pili jina lake Pua, kwamba: Mkiwazalisha wanawake wa Kiebureo waangalieni, wakizaa! Kama mtoto ni wa kiume, sharti mmwue, lakini kama mtoto ni wa kike, na apone! Lakini hao wazalishaji wakamwogopa Mungu, hawakufanya, kama mfalme wa Misri alivyowaagiza, wakawaacha watoto, wapone. Ndipo, mfalme wa Misri alipowaita wale wazalishaji, akawauliza: Mbona mnafanya hivyo mkiwaacha watoto, wapone? Nao wazalishaji wakamwambia Farao: Ni kwa kuwa wanawake wa Kiebureo hawafanani na wanawake wa Kimisri, kwani wao wako na nguvu zaidi, mzalishaji akiwa hajafika bado kwao, wamekwisha kuzaa. Kwa hiyo Mungu akawafanyizia mema hao wazalishaji, nao watu wakaendelea kuwa wengi zaidi wenye nguvu. Kwa kuwa hao wazalishaji walimwogopa Mungu, akawajengea nyumba. Kisha Farao akawaagiza watu wake wote kwamba: Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa sharti mumtupe mtoni, lakini watoto wote wa kike na mwaache, wapone! Mtu wa mlango wa Lawi akaenda, akaoa mwanamke wa Kilawi. Huyo mwanamke akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume; naye alipomwona kuwa mtoto mzuri, akamficha miezi mitatu. Asipoweza kumficha tena, akamchukulia sanduku ya mafunjo, akayaziba kwa udongo wenye utomvu mweusi na kuyapata lami, akamweka mtoto humo ndani; kisha akaiweka hiyo sanduku katika manyasi kando ya mto mkubwa. Umbu lake mtoto akasimama mbali, aone yatakayompata. Mara akatelemka binti Farao, aoge mtoni, vijakazi wake wakitembea kando ya jito. Yeye alipoiona hiyo sanduku katikati ya manyasi akatuma kijakazi wake mmoja kuichukua. Alipoifunua akamwona mtoto, naye huyu kitoto alikuwa akilia; naye akamhurumia, akasema: Ni mtoto wa Waebureo huyu. Ndipo, umbu lake mtoto alipomwuliza binti Farao: Niende kukuitia mnyonyeshaji wa Kiebureo, akunyonyeshee mtoto? Binti Farao akamwambia: Nenda! Ndipo, yule kijana wa kike alipokwenda, akamwita mamake mtoto. Naye binti Farao akamwambia: Mchukue huyu mtoto, uninyonyeshee! Nami nitakupa msahahara wako. Kisha huyo mwanamke akamchukua mtoto, akamnyonyesha. Mtoto alipokuwa mkubwa, akampeleka kwa binti Farao, naye akamwia mwanawe, akamwita jina lake Mose akisema: Kwani nilimtoa majini. Siku zile Mose alipokwisha kukua akatoka kwenda kwa ndugu zake; alipovitazama, walivyofanyishwa kazi ngumu, akaona Mmisri mmoja, akimpiga mmoja wao ndugu zake wa Kiebureo. Ndipo, alipogeuka huko na huko, tena alipoona, ya kama hakuna mtu, akampiga yule Mmisri na kumwua, kisha akamfukia mchangani. Kesho yake alipotoka akaona, wawili wa Kiebureo wakipigana, akamwambia aliye mkorofi: Mbona unampiga mwenzako? Naye akajibu: Yuko nani aliyekuweka kuwa mkuu wa mwamuzi kwetu? Je? Wewe unataka kuniua nami, kama ulivyomwua yule Mmisri? Ndipo, Mose aliposhikwa na woga, akasema: Kumbe lile jambo limejulikana. Farao alipolisikia neno hilo, akamtafuta Mose, amwue; lakini Mose akamkimbia Farao, asimwone, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani, akakaa kwenye kisima. Naye mtambikaji wa Midiani alikuwa na wana wa kike saba; hao walipokuja kuchota maji na kupajaza maji hapo, walipopatengeneza pa kunyweshea mbuzi na kondoo wa baba yao, wakaja wachungaji wengine na kuwafukuza. Ndipo, Mose alipoinuka, akawasaidia akiwanywesha mbuzi na kondoo wao. Walipofika kwa baba yao Reueli, akawauliza: Inakuwaje, mkifika leo, kukiwa mchana bado? Wakasema: Mtu wa Kimisri ametuponya mikononi mwa wale wachungaji, kisha akatuchotea maji, akawanywesha mbuzi na kondoo. Akawauliza wanawe: Yuko wapi? Mbona mmemwacha huko? Mwalikeni, ale nasi! Kisha Mose akapatana kukaa kwake yule mtu, akampa Mose mwanawe Sipora kuwa mkewe. Alipomzalia mtoto wa kiume, akamwita jina lake Gersomu (Mgeni wa Huku), kwani alisema: Nimekuwa mgeni katika nchi isiyo ya kwetu. Siku zilipopita nyingi, yule mfalme wa Misri akafa. Nao wana wa Isiraeli wakapiga kite pamoja na kulia kwa ajili ya utumwa wao, nayo hayo malalamiko yao yakapanda, yakafika kwake Mungu kwa ajili ya huo utumwa wao. Mungu alipoyasikia hayo mauguzi yao, yeye Mungu akalikumbuka Agano lake, alilomwekea Aburahamu na Isaka na Yakobo. Ndipo, Mungu alipowaonea machngu wana wa Isiraeli, kwani yeye Mungu aliwajua, walivyo. Mose alipokuwa akiwachunga mbuzi na kondoo wa mkwewe Yetoro aliyekuwa mtambikaji wa Midiani, akawapitisha mbuzi na kondoo katika hiyo nyika, afike kwenye mlima wa Mungu unaoitwa Horebu. Ndipo, malaika wa Bwana alipomtokea katika moto uliowaka kichakani katikati; naye alipotazama akaona: Kichaka hiki kinawaka moto kweli, lakini kichaka hiki hakiungui. Ndipo, Mose aliposema: Sharti niondoke, nifike hapo, nikione hiki kioja kikubwa, kama ni kwa sababu gani, kichaka hiki kisipoungua. Bwana alipomwona, alivyoondoka, apakaribie kutazama, ndipo, Mungu alipomwita toka hapo kichakani katikati na kusema: Mose! Mose! Akajibu: Mimi hapa! Naye akamwambia: Usifike hapa karibu! Vivue viatu vyako miguuni pako! Kwani mahali hapa, wewe unaposimama, ni nchi takatifu. Kisha akasema: Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Ndipo, Mose alipoufunika uso wake, kwani aliogopa kumwona Mungu. Naye Bwana akasema: Nimeyaona mateso yao walio ukoo wangu walioko Misri, nikasikia, wanavyonililia kwa ajili ya wasimamizi wao wakali, nikayajua maumivu yao. Kwa hiyo nikashuka kuwaponya mikononi mwa Wamisri nikiwatoa katika nchi hiyo na kuwapeleka katika nchi iliyo njema na kubwa, nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali; ndiko, wanakokaa Wakanaani na Wahiti na Waamori na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi. Sasa kwa kuwa vilio vya wana wa Isiraeli vimefika kwangu, nikauona ukorofi, Wamisri wanaowatolea kwa kuwakorofisha, sasa nenda! Ninakutuma kwa Farao, uutoe ukoo wangu wa wana wa Isiraeli huko Misri. Lakini Mose akamwambia Mungu: Mimi ni nani nikienda kwa Farao, niwatoe wana wa Isiraeli huko Misri? Akajibu: Kweli mimi nitakuwa na wewe. Nacho hiki na kiwe kielekezo chako, ya kuwa mimi Mungu nimekutuma: utakapowatoa watu hao huko Misri, mtanitumikia mimi huku mlimani. Mose akamwambia Mungu: Tazama! Nitakapofika kwa wana wa Isiraeli na kuwaambia: Mungu wa baba zenu amenituma kwenu, nao watakaponiuliza: Jina lake nani? nitawaambia nini? Ndipo, Mungu alipomwambia Mose: Nitakuwa niliyekuwa. Akasema: Hivi ndivyo, utakavyowaambia wana wa Isiraeli: Nitakuwa amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Mose: Hivi ndivyo, utakayowaambia wana wa Isiraeli: Bwana, Mungu wa baba zenu aliye Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu. Hili ni Jina langu kale na kale la kunikumbuka kwa vizazi na vizazi. Nenda tu, uwakusanye wazee wa Waisiraeli, uwaambie: Bwana, Mungu wa baba zenu, amenitokea, yeye aliye Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo, akaniambia: Nimewakagua ninyi, nikayaona mnayofanyiziwa huku Misri, nikasema: Nitawatoa ninyi katika mateso ya Misri na kuwapeleka katika nchi yao Wakanaani na Wahiti na Waamori na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi, nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali. Watakapoisikia sauti yako, utakwenda wewe pamoja na wazee wa Waisiraeli kwa mfalme wa Misri, umwambie: Bwana Mungu wa Waebureo amekutana nasi; kwa hiyo sasa tunataka kwenda nyikani safari ya siku tatu, tumtambikie Bwana Mungu wetu. Lakini mimi ninajua, ya kuwa mfalme wa Misri hatawapa ruhusa kwenda zenu, isipokuwa kwa mkono wenye nguvu. Kwa hiyo nitaukunjua mkono wangu, niwapige Wamisri kwa matendo ya kustaajabisha, nitakayoyatenda katikati yao, baadaye atawapa ruhusa kwenda zenu. Lakini wao wa ukoo huu nitawapatia upendeleo machoni pao Wamisri, msiende mikono mitupu hapo, mtakapokwenda, ila kila mwanamke na ajitakie kwa mwenyeji wake na kwa mwenzake wa kukaa naye katika nyumba moja vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu na nguo za kuwavika wana wenu wa kiume na wa kike. Hizi ndizo nyara, mtakazozichukua huko Misri. Mose akajibu kwamba: Lakini hawatanitegemea, wala hawataisikia sauti yangu, kwani watasema: Bwana hakukutokea. Ndipo, Bwana alipomwuliza: Mkononi mwako unashika nini? Akasema: Fimbo. Akamwambia: Itupe chini! Akaitupa chini; ndipo, ilipogeuka kuwa nyoka, naye Mose akamkimbia. Lakini Bwana akamwambia Mose: Upeleke mkono wako, umkamate mkia! Akaupeleka mkono wake na kumkamata, akageuka kuwa fimbo tena mkononi mwake. Hivyo watakutegemea, kwamba amekutuma Bwana Mungu wa baba zao aliye Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Kisha Bwana akamwambia tena: Upeleke mkono wako kifuani pako! Akaupeleka mkono wake kifuani pake; alipoutoa akauona mkono wake kuwa wenye ukoma uliong'aa kama chokaa juani. Kisha akamwambia: Urudishe mkono wako kifuani pako! Alipourudisha mkono wake kifuani pake na kuutoa kifuani pake akauona, ya kuwa umegeuka tena kuwa kama mwili wake. Itakapokuwa, wasikutegemee, wala wasiisikie sauti yako ukifanya kielekezo cha kwanza, wataitegemea sauti yako, utakapokifanya kielekezo cha pili. Lakini itakapokuwa, wasikutegemee, ijapo uvifanye vielekezo viwili, wala wasiisikie sauti yako, basi, chota maji mtoni, uyamwage pakavu! Ndipo, hayo maji, uliyoyachota mtoni, yatakapogeuka kuwa damu hapo pakavu. Lakini Mose akamwambia Bwana: E Bwana wangu! Mimi si mtu ajuaye kusema tangu kale, wala tangu hapo, ulipoanza kusema na mtumishi wako, kwani kinywa changu ni kigumu, nao ulimu wangu ni mzito. Naye Bwana akamwambia: Aliyempa mtu kinywa ni nani? Au ni nani anayemweka mtu kuwa bubu au kiziwi au mwenye macho au kipofu? Si mimi Bwana? Sasa nenda! Nami nitakuwa na kinywa chako, nikufundishe utakayoyasema. Lakini akasema: E Bwana wangu! Tuma utakayemtuma na kumtumia! Ndipo, makali ya Bwana yalipomwakia Mose, akasema: Je? Mkubwa wako Haroni, yule Mlawi, hayuko? Simjui, ya kuwa anajua kabisa kusema? Naye utamwona, akikujia njiani, napo atakapokuona atafurahi moyoni mwake. Useme naye na kuyaweka haya maneno kinywani mwake! Nami nitakuwa na kinywa chako, tena na kinywa chake, niwafundishe ninyi mtakayoyafanya. Yeye ndiye atakayesema nao hao watu, awe kinywa chako, nawe wewe utakuwa kama Mungu wake. Nayo fimbo hii uishike mkononi mwako ya kuvifanyizia vile vielekezo. Ndipo, Mose alipokwenda na kurudi kwake mkwewe Yetoro, akamwambia: Na niende kurudi kwa ndugu zangu walioko Misri, niwatazame, kama wako wazima bado. Yetoro akamwambia Mose: Nenda na kutengemana! Kisha Bwana akamwambia Mose huko Midiani: Nenda kurudi Misri! Kwani wale watu walioitafuta roho yako wamekwisha kufa. Ndipo, Mose alipomchukua mkewe na wanawe, akawapandisha punda, akarudi katika nchi ya Misri; nayo ile fimbo ya Mungu Mose akaichukua mkononi mwake. Naye Bwana akamwambia Mose: Hivyo, unavyokwenda kurudi Misri, viangalie vile vioja vyote, nilivyoviweka mkononi mwako, uvifanye mbele ya Farao! Lakini mimi nitaushupaza moyo wake, asiwape ruhusa hao watu kwenda zao. Ndipo umwambie Farao: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Isiraeli ni mwanangu wa kuzaliwa wa kwanza. Nami ninakuambia: Mpe mwanangu ruhusa, aende zake, apate kunitumikia! Lakini utakapokataa kumpa ruhusa utaniona mimi, nikimwua mwanao wa kuzaliwa wa kwanza. Ikawa njiani, walipokuwa kituoni, Bwana akamjia akitaka kumwua. Ndipo, Sipora alipokamata jiwe lenye makali, akalikata govi la mwanawe, akamgusa nayo miguu yake na kumwambia: Wewe u mchumba wangu aliyekombolewa kwa damu. Ndipo, alipomwacha; lakini hapo akamwita mchumba aliyekombolewa kwa damu kwa ajili ya kule kutahiri. Kisha Bwana akamwambia Haroni: Nenda nyikani kukutana na Mose! Alipokwenda akamkuta penye mlima wa Mungu, akamnonea. Mose akamsimulia Haroni maneno yote ya Bwana, aliyomtuma, navyo vielekezo vyote, alivyomwagiza. Kisha Mose na Haroni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa wana wa Isiraeli. Naye Haroni akayasema maneno yote, Bwana aliyomwambia Mose, navyo vile vielekezo akavifanya machoni pa watu. Ndipo, watu hao walipoyategemea yale maneno; nao waliposikia, ya kuwa Bwana amewakagua wana wa Isiraeli na kuyatazama mateso yao, wakainama na kumwangukia Mungu. Baadaye Mose na Haroni wakaenda, wakamwambia Farao: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli: Hawa watu walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda kunifanyizia sikukuu nyikani! Lakini Farao akasema: Bwana ni nani, nimsikie sauti yake na kuwapa Waisiraeli ruhusa kwenda? Simjui Bwana, wala sitawapa Waisiraeli ruhusa kwenda. Nao wakasema: Mungu wa Waebureo amekutana nasi, kwa hiyo tunataka kwenda nyikani safari ya siku tatu, tumtambikie Bwana Mungu wetu, asitupige kwa magonjwa yauayo wala kwa upanga. Lakini mfalme wa Misri akawaambia: Mbona ninyi Mose na Haroni mnataka kuwatoa tu watu hawa katika kazi zao? Nendeni kuzifanya hizo kazi zenu ngumu! Tena Farao akasema: Tazameni, jinsi watu hawa wa nchi hii walivyo wengi sasa! Nanyi mwataka kuwapumzisha, wasizifanye kazi zao ngumu. Siku ile Farao akawaagiza wale wasimamizi wakali wa hao watu nao waangaliaji wao kwamba: Watu hawa msiwape tena majani makavu ya kuumbia matofali kama siku zote! Sharti waende wenyewe kujiokotea majani makavu. Lakini hesabu ya matofali, waliyoyafanya siku zote, sharti mwabandikie iyo hiyo, msiipunguguze! Kwani ndio walegevu, kwa hiyo hupiga kelele kwamba: Twende kumtambikia Mungu wetu! Kazi za utumwa sharti ziwalemee zaidi watu hawa, wakizifanya, wasitazamie maneno ya uwongo. Ndipo, wasimamizi wale wakali wa watu hao na waangaliaji wao walipowaambia watu kwamba: Hakuna tena atakayewapa ninyi majani makavu; nendeni wenyewe kujiokotea majani makavu po pote, mtakapoyaona! Lakini agano la kazi zenu halipunguki. Ndipo, watu hao walipotawanyika katika nchi nzima ya Misri kuokota majani makavu ya kuumbia matofali. Nao wasimamizi wakawahimiza kwa ukali wao kwamba: Zimalizeni kazi zenu za kuitimiza hesabu yao ya siku zote kama hapo, mlipopewa majani makavu! Nao waangaliaji wana wana wa Isiraeli, wale wasimamizi wakali wa Farao waliowawekea, wakapigwa kwa kwamba: Mbona hamkulitimiza jana na leo agano lenu la matofali la siku zote? Ndipo, waangaliaji wa wana wa Isiraeli walipokuja, wakamlilia Farao kwamba; Mbona unawafanyizia watumwa wako hivyo? Majani makavu watumwa wako hawapewi, lakini wanatuambia: Fanyeni matofali yayo hayo! Nasi watumwa wako tunapigwa, lakini wenye kukosa ni watu wako. Lakini akasema: Ninyi m walegevu, m walegevu kweli. Kawa sababu hii mnasema: Twende, tumtambikie Bwana! Sasa haya! Nendeni kuzifanya kazi zenu! Majani makavu hamtapewa, ila hesabu ya matofali iliyowekwa sharti mwitoe! Nao waangaliaji wa wana wa Isiraeli wakajiona, ya kuwa wamepatwa na mabaya kwa kuambiwa: Msiipunguze hesabu ya matofali ya siku zote! Walipotoka kwake Farao, wakamkuta Mose na Haroni waliosimama hapo na kuwangoja. Ndipo, walipowaambia: Bwana na awatazame ninyi, mlivyo, awapatilize! Kwani mmeufanya mnuko wetu kuwa mbaya puani mwake Farao namo puani mwao watumishi wake, mkawapa panga mikononi mwao, watuue. Naye Mose akamrudia Bwana na kusema: Bwana, kwa nini unawafanyia watu hawa mabaya kama hayo? Ndiyo haya, uliyonituma? Kwani tangu hapo, nilipoingia kwake Farao kusema naye katika Jina lako, amezidi kuwafanyizia watu hawa mabaya, wewe nawe hukuwaponya kabisa wao walio ukoo wako. Bwana akamwambia Mose: Sasa utayaona, nitakayomfanyizia Farao, kwani kwa mkono wenye nguvu atawapa ruhusa kwenda zao, tena kwa huo mkono wenye nguvu atawakimbiza, waitoke nchi yake. Kisha Bwana akasema na Mose, akamwambia: Mimi ni Bwana. Nilimtokea Aburahamu na Isaka na Yakobo, wanijue kuwa Mungu Mwenyezi, lakini Jina langu la Bwana sikulijulisha kwao. Nalo Agano langu, nililolifanya nao, nitalisimamisha, lile la kuwapa nchi ya Kanaani, ndiyo nchi, waliyoikaa ugeni ni kwani walikuwa wageni huko. Nami niliposikia, wana wa Isiraeli wanavyopiga kite kwa hivyo, Wamisri wanavyowafanyizisha kazi za utumwa, nimelikumbuka hilo Agano langu. Kwa sababu hii waambie wana wa Isiraeli: Mimi ni Bwana, mimi nitawatoa Misri na kuwatua mizigo yenu, mimi nitawatoa utumwani mwenu na kuwakomboa ninyi kwa kuukunjua mkono na kwa mapatilizo makubwa. Nami nitawachukua ninyi, mwe ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtatambua, ya kuwa mimi Bwana ni Mungu wenu aliyewatoa Misri na kuwatua mizigo yenu. Nami nitawapeleka katika hiyo nchi, niliyoiapia na kuuinua mkono wangu kwamba: Nitampa Aburahamu na Isaka na Yakobo; hiyo ndiyo, mimi Bwana nitakayowapa ninyi, iwe yenu. Mose alipowaambia wana wa Isiraeli maneno haya, hawakumsikia Mose, kwa kuwa roho zao zilikuwa zimesongeka, kazi zikizidi kuwa ngumu. Kisha Bwana akamwambia Mose kwamba: Nenda, useme na Farao, mfalme wa Misri, awape wana wa Isiraeli ruhusa kutoka katika nchi yake! Lakini Mose akamwambia Bwana waziwazi kwamba: Tazama! Wana wa Isiraeli wasiponisikia, Farao atanisikiaje mimi niliye mwenye midomo isiyofunguliwa kusema vema? Kisha Bwana akasema nao Mose na Haroni akiwaagiza kwenda kwa wana wa Isiraeli na kwa Farao, mfalme wa Misri, wapate kuwatoa wana wa Isiraeli katika nchi ya Misri. Hawa ndio vichwa vya milango ya baba zao: Wana wa Rubeni aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Isiraeli ndio hawa: Henoki na Palu, Hesironi na Karmi. Hizi ndizo ndugu zao wa Rubeni. Nao wana wa Simeoni ndio hawa: Yemueli na Yamini na Ohadi na Yakini na Sohari na Sauli, mwana wa mke wa Kikanaani. Hizi ndizo ndugu zao wa Simeoni. Nayo haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, kama walivyofuatana kuzaliwa: Gersoni na Kehati na Merari, nayo miaka ya kuwapo kwake Lawi ilikuwa miaka 137. Wana wa Gersoni ni Libuni na simei kwa udugu wao. Nao wana wa Kehati ni Amuramu na Isihari na Heburoni na Uzieli; nayo miaka ya kuwapo kwake Kehati ilikuwa miaka 133. Nao wana wa Merari ni Mahali na Musi; hizi ndio ndugu zao Walawi kwa hiyo, walivyofuatana kuzaliwa. Naye Amuramu akaamchukua Yokebedi aliyekuwa shangazi yake kuwa mkewe, naye akamzalia Haroni na Mose; nayo miaka ya kuwapo kwake Amuramu ilikuwa miaka 137. Nao wana wa Isihari ni Kora na Nefegi na Zikiri. Nao wana wa Uzieli ni Misaeli na Elsafani na Sitiri. Naye Haroni akamchukua Eliseba, binti Aminadabu, umbu lake Nasoni, kuwa mkewe, naye akamzalia Nadabu na Abihu na Elazari na Itamari. Nao wana wa Kora ni Asiri na Elkana na Abiasafu. Hizi ndizo ndugu zao Wakora. Naye Elazari, mwana wa Haroni, akachukua mmoja wao wana wa Putieli kuwa mkewe, naye akamzalia Pinehasi. Hawa ndio vichwa vya milango ya baba zao Walawi kwa udugu wao. Yule Haroni naye yule Mose ndio, Bwana aliowaambia: Watoeni wana wa Isiraeli katika nchi hii ya Misri kikosi kwa kikosi! Wao ndio waliosema na Farao, mfalme wa Misri, wapate kuwatoa wana wa Isiraeli huko Misri, yeye Mose naye Haroni. Ikawa siku hiyo, Bwana aliposema na Mose huko Misri, ndipo, Bwana alipomwambia Mose kwamba: Mimi ni Bwana; mwambie Farao, mfalme wa Misri, yote, mimi nitakayokuambia; tena ndipo hapo, Mose alipomwambia Bwana waziwazi: Tazama, mimi ni mwenye midomo isiyofunguliwa kusema vema; kwa hiyo Farao atanisikiaje? Kisha Bwana akamwambia Mose: Tazama, nimekupa kuwa kama Mungu kwake Farao, naye kaka yako Haroni atakuwa mfumbuaji wako. Wewe na uyaseme yote, nitakayokuagiza, naye kaka yako Haroni na amwambie Farao, awape wana wa Isiraeli ruhusa kutoka katika nchi yake. Lakini mimi nitaushupaza moyo wake Farao, nipate kufanya vielekezo na vioja vyangu vingi katika nchi ya Misri. Farao asipowasikia ninyi, nitautokeza mkono wangu huko Misri; ndivyo, nitakavyowatoa vikosi vyangu walio ukoo wangu wa wana wa Isiraeli katika nchi ya Misri kwa mapatilizo makubwa. Wamisri nao watambue, ya kuwa Bwana ni mimi. Itakuwa hapo, nitakapowakunjulia Wamisri mkono wangu, nipate kuwatoa wana wa Isiraeli katikati yao. Mose na Haroni wakafanya, kama Bwana alivyowaagiza; hivyo ndivyo, walivyofanya. Mose alikuwa mwenye miaka 80, naye Haroni alikuwa mwenye miaka 83, waliposema Farao. Bwana akamwwambia Mose na Haroni kwamba: Farao atakapowaambia: Fanyeni kioja, niwajue, mwambie Haroni: Ikamate fimbo yako, uitupe chini mbele ya Farao, iwe nyoka! Mose na Haroni walipofika kwake Farao wakafanya hivyo, kama Bwana alivyowaagiza: Haroni alipoitupa fimbo yake chini mbele yake Farao na mbele yao watumishi wake, ikawa nyoka. Ndipo, Farao naye alipowaita wajuzi na walozi, nao hao waganga wakafanya hivyo kwa uganga wao. Wakazitupa fimbo zao chini, kila mtu yake, nazo zikawa nyoka, lakini fimbo yake Haroni ikazimeza fimbo zao. Moyo wake Farao ukashupaa, asiwasikie, kama Bwana alivyosema. Bwana akamwambia Mose: Moyo wa Farao ni mgumu, anakataa kuwapa watu hawa ruhusa kwenda zao. Kesho asubuhi nenda kwa Farao, utakapomwona, akitoka kwenda majini! Nawe simama hapo ukingoni kwa mto na kumngoja ukiishika mkononi mwako ile fimbo iliyogeuka kuwa nyoka! Nawe umwambie: Bwana Mungu wa Waebureo amenituma kwako kukuambia: Hao watu walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda zao, wanitumikie nyikani! Lakini mpaka hapa hujasikia bado. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa hili na utambue, ya kuwa mimi ni Bwana: Tazama! Mimi nitakapoyapiga maji yaliyomo humu mtoni kwa fimbo hii, ninayoishika mkononi, ndipo, yatakapogeuka kuwa damu. Nao samaki waliomo humu mtoni watakufa, nao mto utanuka vibaya, nao Wamisri watachukizwa kuyanywa maji ya mtoni. Kisha Bwana akamwambia Mose: Mwambie Haroni: Ichukue fimbo yako, kisha ukunjue mkono wako na kuuelekezea maji yao ya Misri yaliyomo vijitoni namo majitoni namo maziwani namo mashimoni, maji yanamokusanyika, yageuke kuwa damu! ndipo, yatakapogeuka kuwa damu katika nchi yote nzima ya Misri, nayo yaliyomo katika vyombo vya miti namo katika vyombo vya mawe. Mose na Haroni wakafanya hivyo, kama Bwana alivyoagiza. Haroni alipoinyanyua hiyo fimbo na kuyapiga maji yaliyomo humo mtoni machoni pake Farao napo machoni pao watumishi wake, ndipo, maji yote yaliyomo humo mtoni yalipogeuzwa kuwa damu. Nao samaki waliokuwamo mtoni wakafa, nao mto ukanuka vibaya, Wamisri wasiweze kuyanywa hayo maji ya mtoni, maana yote yaligeuka kuwa damu katika nchi nzima ya Misri. Lakini waganga wa Misri wakavifanya nao kwa uganga wao; ndipo, moyo wake Farao uliposhupaa, asiwasikie, kama Bwana alivyosema. Kisha Farao akageuka, akaingia nyumbani mwake, pasipo kuviweka moyoni mwake. Wamisri wote wakachimba maji pande zote za mtoni, wapate ya kunywa, kwani maji ya mtoni hawakuweza kuyanywa. Vikawa hivyo siku saba zote, Bwana alipokwisha kuupiga huo mto. Kisha Bwana akamwambia Mose: Nenda kwa Farao, umwambie: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Watu hawa walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda zao, wanitumikie! Lakini wewe utakapokataa kuwapa ruhusa kwenda zao, utaniona mimi, nikiipiga mipaka yako yote na kuleta vyura, huo mto ufurikiwe na vyura, nao watapanda, waingie nyumbani mwako namo chumbani mwako mwa kulalia, hata kitandani pako, namo nyumbani mwao watumishi wako, namo vijumbani mwao watu wako, namo majikoni mwako, namo mabakulini mwa kutengenezea mikate. Kisha watapanda hao vyura namo mwilini mwako, namo miiilini mwa watu wako wote, namo miilini mwa watumishi wako wote. Kisha Bwana akamwambia Mose: Mwambie Haroni: Ukunjue mkono wako wenye fimbo yako na kuuelekezea vijito na mito na maziwa, upandishe vyura, waijie nchi ya Misri. Haroni alipoukunjua mkono wake na kuuelekezea maji ya Misri, ndipo, vyura walipopanda, wakaifunika nchi ya Misri. Waganga nao wakavifanya kwa uganga wao, wakapandisha vyura, waijue nchi ya Misri. Ndipo, Farao alipomwita Mose na Haroni, akawaambia: Niombeeni kwa Bwana, awaondoe hawa vyura kwangu na kwa watu wangu! Ndipo, nitakapowapa ruhusa watu wa ukoo huu kwenda zao, wamtambikie Bwana. Mose akamwambia Farao: Kwa utukufu wako niambie sawasawa, kama ni lini, unapotaka, niwaombee ninyi, wewe na watumishi wako na watu wako, hawa vyura waondolewe kabisa kwako namo manyumbani mwako, wasalie mtoni tu. Akasema: Kesho. Akajibu: Itakuwa, kama ulivyosema, upate kujua, ya kuwa hakuna anayefanana na Bwana Mungu wetu. Hawa vyura wataondoka kwako na manyumbani mwako, namo mwao watumishi wako, namo mwao watu wako, wasalie mtoni tu. Kisha Mose na Haroni wakatoka kwake Farao, naye Mose akamlilia Bwana kwa ajili ya hao vyura, aliompatia Farao. Bwana akafanya, kama Mose alivyosema: vyura wakafa manyumbani na nyuani na mashambani, wakawakusanya machungu machungu, nchi ikanuka vibaya. Lakini Farao alipoona, ya kuwa jambo limetulia, akaushupaza moyo wake, asiwasikie, kama Bwana alivyosema. Kisha Bwana akamwambia Mose: Mwambie Haroni: Inyanyue fimbo yako, uyapige mavumbi ya chini, yageuke kuwa mbu katika nchi yote ya Misri! Wakafanya hivyo; Haroni alipoukunjua mkono wake wenye fimbo yake na kuyapiga mavumbi ya chini, yakageuka kuwa mbu, wakawauma watu na nyama; mavumbi yote ya nchi yakageuka kuwa mbu katika nchi yote ya Misri. Waganga nao walipofanya hivyo, watokeze mbu kwa uganga wao, hawakuweza; nao wale mbu wakawauma watu na nyama. Ndipo, walipomwambia Farao: Hiki ndicho kidole chake Mungu! Lakini moyo wake Farao ukashupaa, asiwasikie, kama Bwana alivyosema. Bwana akamwambia Mose: Kesho asubuhi na mapema ujidamke, upate kumtokea Farao, utakapomwona, akitoka kwenda majini! Ndipo umwambie: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Watu hawa walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda zao, wanitumikie! Hawa watu walio ukoo wangu usipowapa ruhusa kwenda zao, utaniona, nikituma kwenu, wewe na watumishi wako na watu wako, namo manyumbani mwako mainzi wabaya, nyumba za Misri nazo nchi, wanazozikaa, zijae hao mainzi wabaya. Lakini nchi ya Goseni, wao walio ukoo wangu wanayoikaa, nitaitenga siku hiyo, hao mainzi wabaya wasiweko huko, kusudi upate kujua, ya kuwa mimi Bwana niko katikati ya nchi hiyo. Hivyo nitawatenga wao walio ukoo wangu nao walio wako; hiki kielekezo kitafanyika kesho. Bwana akavifanya hivyo: mainzi wabaya na wakubwa wakaingia nyumbani mwa Farao namo manyumbani mwa watumishi wake na katika nchi yote ya Misri, nayo nchi ikaharibika kwa ajili ya hao mainzi wabaya. Ndipo, Farao alipomwita Mose na Haroni, akawaambia: Nendeni kumtambikia Mungu wenu katika nchi hii! Lakini Mose akamwambia: Haiwezekani kuvifanya hivyo; kwani tukimtambikia Bwana Mungu wetu, ingewachukiza Wamisri; nao watakapotuona, tukichinja machoni pao ng'ombe za tambiko zinazowachukiza, hawatatupiga mawe? Sharti twende nyikani safari ya siku tatu, tupate kumtambikia Bwana Mungu wetu, kama alivyotuambia. Ndipo, Farao aliposema: Basi, mimi nitawapa ninyi ruhusa kwenda kumtambikia Bwana Mungu wenu nyikani. Ninataka hili tu: msiende mbali zaidi, tena: mniombee. Naye Mose akasema: Tazama! Nikitoka kwako nitamwomba Bwana, hawa mainzi wabaya waondoke kesho kwake Farao nako kwao watumishi wake na watu wake, lakini Farao asiendelee kutudanganya, akikataa tena kuwapa hawa watu ruhusa kwenda zao, wapate kumtambikia Bwana! Mose alipotoka kwake Farao, akamwomba Bwana. Naye Bwana akafanya, kama Mose alivyosema: Wale mainzi wabaya wakaondoka kwake Farao nako kwao watumishi wake na watu wake, hakusalia hata mmoja. Lakini Farao akaushupaza moyo wake nayo mara hii, hakuwapa hao watu ruhusa kwenda zao. Bwana akamwambia Mose: Nenda kwa Farao, umwambie: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Waebureo: Watu hawa walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda zao, wanitumikie! Lakini utakapokataa kuwapa ruhusa na kuwashika tena, ndipo, utakapouona mkono wa Bwana, ukiyajia makundi ya mashambani, farasi na punda na ngamia na ng'ombe na mbuzi na kondoo, wapatwe na kidei kikali sana. Naye Bwana atayapambanua makundi ya Waisiraeli nayo makundi ya Wamisri, nao nyama wote pia walio wao Waisiraeli hatakufa hata mmoja wao. Bwana akaweka muda kwamba: Kesho Bwana atalifanya jambo hilo katika nchi hii. Kesho yake Bwana akalifanya kweli hilo jambo, wakafa nyama wa makundi yote ya Misri, lakini miongoni mwa makundi ya wana wa Isiraeli hakufa nyama hata mmoja. Farao alipotuma watu kutazama, wakaona, ya kuwa katika makundi ya Waisiraeli hakufa nyama hata mmoja. Lakini moyo wake Farao ukawa mgumu, hakuwapa hao watu ruhusa kwenda zao. Bwana akamwambia Mose na Haroni: Jichukulieni majivu ya jikoni ya kuyajaza magao yenu! Kisha Mose ayasambaze juu angani machoni pake Farao. Ndipo, mavumbi yake membamba yatakapoieneza nchi yote ya Misri na kuwapata watu na nyama, watokewe na majipujipu ya ndui katika nchi yote ya Misri. Ndipo, walipochukua majivu ya jikoni, wakaenda kusimama mbele ya Farao; ndipo, Mose alipoyasambaza juu angani, mara majipujipu ya ndui yakawatoka watu na nyama. Nao wale waganga hawakuweza kusimama mbele ya Mose kwa ajili ya hayo majipujipu, kwani hayo majipujibu yaliwapata wale waganga nao pamoja na Wamisri wote. Lakini Bwana akaushupaza moyo wa Farao, asiwasikie, kama Bwana alivyomwambia Mose. Bwana akamwambia Mose: Kesho asubuhi na mapema ujidamke, upate kumtokea Farao na kumwambia: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Waebureo: Watu hawa walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda zao! Kwani mara hii nitayatuma mapigo yangu yote, yakupate wewe moyoni mwako nao watumishi wako pamoja na watu wako, kusudi upate kujua, ya kuwa hakuna aliye kama mimi humu ulimwenguni mote. Kwani ningaliweza kuunyosha mkono wangu, ukupige wewe pamoja na watu wako kwa magonjwa yauayo, ukatoweka katika nchi hii; lakini nikikuweka, ni kwa sababu hiihii, nipate kukuonyesha nguvu zangu, Jina langu lipate kutangazwa katika nchi zote. Ukiendelea kuwapingia wao walio ukoo wangu, usiwape ruhusa kwenda zao, utaniona, nikinyesha kesho saa zizi hizi mvua ya mawe mazito sana, isiyokuwa bado huku Misri yenye nguvu kama hiyo tangu siku ile, misingi yake ilipowekwa, hata sasa. Sasa tuma watu, wayahimize makundi yako nao wote wa kwako walioko mashambani kukimbilia nyumbani! Kwani watu wote, nao nyama wote watakaoonekana mashambani, wasiopelekwa nyumbani watakufa, mvua hiyo ya mawe itakapowanyeshea. Ndipo, wao walioliogopa hilo neno la Bwana miongoni mwa watumishi wa Farao walipowakimbiza watumwa wao na makundi yao na kuwingiza nyumbani. Lakini wasioliweka hilo neno la Bwana mioyoni mwao wakawaacha watumwa wao na makundi yao mashambani. Kisha Bwana akamwambia Mose: Unyoshe mkono wako na kuuelekeza mbinguni, mvua ya mawe inyeshe katika nchi yote ya Misri na kuwapiga watu na nyama na majani yote yaliyoko mashambani katika nchi ya Misri! Mose alipoiinua fimbo yake na kuielekeza mbinguni, ndipo, Bwana alipopiga ngurumo na kunyesha mvua ya mawe, moto wa umeme ukaanguka chini. Ndivyo, Bwana alivyonyesha mvua ya mawe katika nchi ya Misri. Hiyo mvua ya mawe iliponyesha, moto ulichanganyika nayo hiyo mvua ya mawe mazito sana isiyokuwa bado katika nchi yote ya Misri yenye nguvu kama hiyo tangu hapo, watu walipoanza kukaa huko. Hiyo mvua ya mawe ikapiga katika nchi yote ya Misri yote pia yaliyokuwako mashambani, watu na nyama, nayo majani ya mashambani ikayapiga hiyo mvua ya mawe, ikaivunja nayo miti yote ya mashambani. Katika nchi ya Goseni tu, wana wa Isiraeli walikokaa, hiyo mvua ya mawe haikuwako. Ndipo, Farao alipotuma watu kumwita Mose na Haroni, akawaambia: Mara hii nimekosa; kwani Bwana ni mwongofu, lakini mimi na watu wangu tu wapotovu. Niombeeni kwa Bwana, hizi ngurumo za Mungu zikome pamoja na mvua ya mawe kwa kuwa nyingi mno! Kisha nitawapa ninyi ruhusa kwenda zenu, msikae huku tena siku nyingi. Naye Mose akamwambia: Nitakapotoka humu mjini nitamwinulia Bwana mikono yangu, ndipo, hizi ngurumo zitakapokoma, nayo hii mvua ya mawe haitakunya tena, kusudi mpate kujua, ya kuwa nchi ni yake Bwana. Lakini ninakujua wewe nao watumishi wako, ya kama hamjapata kumwogopa Bwana Mungu. Hivyo ndivyo, mipamba na miwele ilivyopigwa, kwani miwele ilikuwa imekwisha kuchanua, nayo mipamba ilikuwa imekwisha kuzaa. Lakini ngano na mtama hazikupigwa, kwa kuwa zilikuwa hazijaota bado. Mose alipotoka mle mjini mwake Farao, akamwinulia Bwana mikono yake; ndipo, ngurumo na mvua ya mawe zilipokoma, hata mvua haikunyesha tena katika nchi hiyo. Lakini Farao alipoona, ya kama mvua na mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akaendelea kukosa, akaushupaza moyo wake, yeye nao watumishi wake. Moyo wake Farao ukawa mgumu, asiwape wana wa Isiraeli ruhusa kwenda zao, kama Bwana alivyosema kinywani mwa Mose. Bwana akamwambia Mose: Nenda kwake Farao! Kwani mimi nimeushupaza moyo wake nayo mioyo ya watumishi wake, nipate kuvitoa hivi vielekezo vyangu katikati yao, kusudi wewe uyasimulie masikioni mwa mwanao namo mwa mjukuuu wako, niliyoyafanya huku Misri, navyo vilekezo vyangu, nilivyoviweka kwao, mpate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana. Mose na Haroni walipofika kwake Farao wakamwambia: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Waebureo: Mpaka lini utakataa kujinyenyekeza usoni pangu? Watu hawa walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda zao, wanitumikie! Kwani utakapokataa kuwapa ruhusa kwenda zao walio ukoo wangu, utaniona, nikileta nzige kesho katika mipaka yako. Nao wataifunika nchi hapo juu, watu wasiweze kuona mchanga, nao watayala masazo yenu yote yaliyosazwa kwa kuiponea mvua ya mawe, nayo miti yenu yote iliyochipuka tena wataila mashambani. Watajaa namo nyumbani mwako namo manyumbani mwa watumishi wako, namo manyumbani mwa Wamisri wote; ajabu kama hilo hawakuliona baba zako, wala baba za baba zako tangu hapo, walipoanza kuwapo katika nchi hii hata siku hii ya leo. Kisha akageuka, akatoka kwake Farao. Ndipo, watumishi wake Farao walipomwambia: Mpaka lini mtu huyu atatunasa? Watu hawa wape ruhusa kwenda zao, wamtumikie Bwana Mungu wao! Hujatambua bado, ya kuwa Misri imekwisha kuangamia? Kwa hiyo Mose na Haroni wakarudishwa kwake Farao, naye akawaambia: Nendeni kumtumikia Bwana Mungu wenu! Lakini watakaokwenda ni nani na nani? Mose akajibu: Tunakwenda vijana wetu na wazee wetu, wana wetu wa kiume na wa kike, nao mbuzi na kondoo wetu na ng'ombe wetu tutakwenda nao, kwani tuna sikukuu ya Bwana. Lakini akawaambia: Ehe! Bwana na awe nanyi vivyo hivyo, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu! Yatazameni mabaya, mliyo nayo, myafuate! Hivyo sivyo! Ila nendeni ninyi waume kumtumikia Bwana! Kwani hii ndiyo, mnayoitaka. Kisha wakawafukuza, watoke usoni pake Farao. Ndipo, Bwana alipomwambia Mose: Uinue mkono wako juu ya nchi ya Misri, nzige waje! Nao na waiingie nchi ya Misri, wale majani yote ya nchi hii nayo yote pia, mvua ya mawe iliyoyasaza. Mose alipoiinua fimbo yake juu ya nchi ya Misri, Bwana akaleta upepo toka maawioni kwa jua, nao ukavuma katika nchi hiyo mchana kutwa na usiku kucha; kulipokucha, huo upepo wa maawioni kwa jua ulikuwa umewaleta nzige. Nao hawa nzige wakaiingia nchi yote ya Misri, wakatua po pote katika mipaka ya Misri, nao walikuwa wakali sana wa kula; nzige kama hao walikuwa hawajatokea siku zilizopita, wala hawatatokea siku zijazo. Wakaifunikiza nchi yote pia hapo juu, hata nchi ikapata giza; wakayala majani yote ya nchi nayo matunda yote ya miti, mvua ya mawe iliyoyasaza, hakukusalia jani moja tu penye miti wala penye vijiti vya mashambani katika nchi yote ya Misri. Ndipo, Farao alipomwita kwa upesi Mose na Haroni, akawaambia: Nimemkosea Bwana Mungu wenu, hata ninyi. Sasa uniondolee nayo mara hii kosa langu, mniombee kwa Bwana Mungu wenu, aniondolee kifo hiki tu! Alipotoka kwake Farao, akamwomba Bwana. Ndipo, Bwana alipoleta upepo mwingine toka baharini wenye nguvu sana, ukawainua wale nzige, ukawapeleka na kuwatosa katika Bahari Nyekundu, asisalie nzige hata mmoja katika mipaka yote ya Misri. Kisha Bwana akaushupaza moyo wa Farao, asiwape wana wa Isiraeli ruhusa kwenda zao. Bwana akamwambia Mose: Uinue mkono wako na kuuelekeza mbinguni, katika nchi ya Misri kuwe giza jeusi sana la kupapaswa. Mose alipouinua mkono wake na kuuelekeza mbinguni, kukawa na giza nene katika nchi yote ya Misri siku tatu. Mtu hakuweza kumwona mwenziwe, wala mtu hakuondoka siku tatu mahali, alipokuwa. Lakini kwao wana wa Israeli kulikuwa na mwanga po pote, walipokaa. Ndipo, Farao alipomwita Mose, akamwambia: Nendeni kumtumikia Bwana! Mbuzi na kondoo na ng'ombe tu waachwe huku, lakini wana wenu na waende nayi! Mose akamwambia: Sharti wewe mwenyewe utupe mikononi mwetu ng'ombe za tambiko za kuchinja nazo za kuteketeza nzima, tupate za kumtolea Bwana Mungu wetu. Kwa hiyo, nayo makundi yetu sharti yaende nasi, lisisalie hata kwato moja. Kwani humo ndimo, tutakamochukua za kumtambikia Bwana Mungu wetu; kwani sisi hatujui, jinzi tutakavyomtumikia Bwana, mpaka tufike huko. Lakini Bwana akaushupaza moyo wa Farao, akatae kuwapa ruhusa kwenda zao. Kwa hiyo Farao akamwambia: Ondoka kwangu! Jiangalie, usitokee tena kuuona uso wangu! Kwani siku, utakapouona uso wangu, utakufa. Mose akajibu: Na viwe hivyo, ulivyosema, nisiuone tena uso wako mara nyingine. Bwana akamwambia Mose: Liko pigo moja bado, nitakalompatia Farao nao Wamisri, baadaye atawapa ninyi ruhusa kutoka huku; naye hapo, atakapowapa ruhusa kwenda zenu na mali zenu zote, atawakimbiza ninyi kabisa kuondoka huku. Kwa hiyo sema masikioni mwa watu hawa, waombe vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu kila mtu kwa mwenziwe, hata kila mwanamke kwa mwenziwe. Bwana atawapatia hawa watu upendeleo machoni pao Wamisri, maana huyo Mose alikuwa mkubwa sana katika nchi ya Misri machoni pao watumishi wa Farao napo machoni pa watu. Mose akasema: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana: Usiku wa manane nitatokea katikati ya nchi ya Misri; ndipo, kila mwana wa kwanza atakapokufa katika nchi ya Misri, kuanzia mwana wa kwanza wa Farao anayekaa katika kiti chake cha kifalme, kuishia mwana wa kwanza wa kijakazi anayekaa penye mawe ya kusagia, hata kila mwana wa kwanza wa nyama wa kufuga. Ndipo, maombolezo yatakapokuwa makuu katika nchi yote ya Misri yasiyokuwa bado siku zilizopita, wala hayatakuwa kama hayo siku zijazo. Lakini kwa wana wote wa Isiraeli mbwa tu hatakemea wala mtu wala nyama, kusudi mpate kujua, ya kuwa Bwana huwapambanua Wamisri na Waisiraeli. Ndipo, hawa watumishi wako wote watakapotelemka, waje kwangu na kuniangukia kwamba: Toka wewe na hawa watu wote wanaozifuata nyayo zako! Ndipo, nitakapotoka. Kisha Mose akatoka kwake Farao kwa kuwa na ukali uliowaka moto. Kisha Bwana akamwambia Mose: Farao hatawasikia ninyi, kusudi vifanyike vioja vyangu vingi katika nchi ya Misri. Nao Mose na Haroni walipovifanya hivyo mbele ya Farao, Bwana akaushupaza moyo wa Farao, asiwape wana wa Isiraeli ruhusa kutoka katika nchi yake. Bwana akamwambia Mose na Haroni katika nchi ya Misri kwamba: Mezi huu sharti uwawie wa kwanza a miezi, uwe wenu wa kwanza wa kuihesabu miezi ya mwaka. Uambieni mkutano wote wa wana wa Isiraeli kwamba: Siku ya kumi ya mwezi huu kila mwenye nyumba na achukue mwana kondoo, watu wa kila nyumba moja mwana kondoo mmoja! Lakini kama watu wa nyumba moja ni wachache, wsiweze kumaliza mwana kondoo, basi, yeye na jirani yake wa kukaa karibu ya nyumba yake watachukua mmoja kwa hesabu yao waliomo humo nyumbani; kwa hivyo, watu wanavyoweza kula, na mmhesabie mwana kondoo watu wa kumla. Nanyi na mchukue mwana kondoo asiye na kilema, aliye wa kiume mwenye mwaka mmoja, akiwa mwana kondoo au mwana mbuzi. Na mwe naye na kumwangalia mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi huu; ndipo watu wote pia wa mkutano wa Waisiraeli wamchinje saa za jioni. Nayo damu yake ya kutosha na wachukue ya kuipaka miimo yote miwili ya mlango na kizingiti cha juu katika hizo nyumba, watakamolia. Usiku uleule na wazile nyama zake, nazo ziwe zimechomwa motoni. Na wazile pamoja na mikate isiyochachwa na pamoja na mboga chungu. Msizile, zikiwa mbichi, wala zikiwa zimepikwa majini, ila sharti ziwe zimechomwa nzima motoni, kichwa kikiwa pamoja na paja zake na utumbo wake. Wala mzisaze nyama nyingine hata asubuhi! Ila zitakazosalia hata asubuhi mziteketeze kwa moto! Tena hivi ndivyo, mtakavyozila: Viuno vyenu na viwe vimefungwa, namo miguuni mwe mmevaa viatu, nazo fimbo zenu na mzishike mikononi mwenu. Hivyo mzile kama watu wanaojihimiza kwenda safari. Kwani hii ndio Pasaka ya Bwana. Nami nitapita usiku uleule katika nchi yote ya Misri, nimpige kila mwana wa kwanza katika nchi ya Misri aliye wa wwatu pamoja nao walio wa nyama wa kufuga, nayo miungu yote ya Misri nitaihukumu mimi Bwana. Nazo zile damu penye nyumba mlimo zitakuwa kielekezo chenu: nitakapoziona nitapita kwenu, lisiwapate ninyi lile pigo la mwangamizaji, nitakapoipiga nchi ya Misri. Siku hiyo sharti iwe kwenu ya kuikumbuka, mwilie sikukuu ya Bwana. Haya na yawe maongozi ya kale na kale kwa vizazi vyenu vijvyo, mwilie sikukuu. Siku saba na mle mikate isiyochachwa. Siku ya kwanza sharti mkomeshe chachu na kuziondoa nyumbani mwenu, kwani kila atakayekula siku ya kwanza mpaka siku ya saba yaliyo yenye chachu sharti huyo ang'olewe kwao Waisiraeli. Siku ya kwanza sharti mkutanie Patakatifu, nayo siku ya saba mkutanie Patakatifu; siku hizo zisifanywe kazi zo zote, kazi iliyo na ruhusa kwenu peke yake tu ni hiyo ya chakula cha kila mtu. Iangalieni hiyo mikate isiyochachwa! Kwani siku hiyo ndipo papo hapo, nilipovitoa vikosi vyenu katika nchi ya Misri. Kwa hiyo iangalieni siku hiyo! Haya na yawe maongozi ya kale na kale kwa vizazi vyenu vijavyo. Siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza jioni na mle mikate isiyochachwa mpaka jioni ya siku ya ishirini na moja ya mwezi huo. Siku saba chachu isionekane nyumbani mwenu, kwani kila atakayekula iliyo yenye chache siku hizo sharti huyo ang'olewe katika mkutano wa Waisiraeli, kama ni mgeni, au kama ni mzalia wa nchi hiyo. Msile cho chote chenye chachu siku hizo, ila po pote, mtakapokaa, sharti mle mikate isiyochachwa. Mose akawaita wazee wote wa Waisiraeli, akawaambia: Haya! Nendeni, mchukue wana kondoo wa kuwatoshea ndugu wa nyumbani mwenu, mwachinje kuwa wa Pasaka! Tena chukueni vitita vya vivumbasi, mvichovye katika damu iliyotiwa katika bakuli, mkinyunyizie kizingiti cha juu na miimo yote miwili ya mlango hiyo damu iliyotiwa katika bakuli, tena mtu ye yote wa kwenu asitoke mlangoni mwa nyumbani mwake, mpaka kuche. Naye Bwana atapita kuwapiga wana wa kwanza wa Misri; hapo, atakapoona damu penye kizingiti cha juu na penye miimo yote miwili, basi, Bwana ataupita mlango huo, asimpe mwangamizaji ruhusa kuingia nyumbani mwenu na kuwapiga. Nalo neno hili sharti mliangalie kuwa maongozi yako na ya wanao kale na kale. Napo hapo, mtakapoingia katika hiyo nchi, Bwana atakayowapa, kama alivyosema, sharti mwuangalie utumishi huu. Tena hapo, wana wenu watakapowauliza: Huu utumishi wenu maana yake nini? na mwaambie: Hii ndio ng'ombe ya tambiko ya Pasaka ya Bwana, kwa kuwa alizipita nyumba za wana wa Isiraeli huko Misri, akaziponya nyumba zetu alipowapiga Wamisri. Ndipo, watu walipoinama na kumwangukia Mungu. Kisha wana wa Isiraeli wakaenda, wakafanya, kama Bwana alivyomwagiza Mose na Haroni; hivyo ndivyo, walivyofanya. Ulipokuwa usiku wa manane, Bwana akawapiga wana wa kwanza wote katika nchi ya Misri, kuanzia mwana wa kwanza wa Farao aliyekaa katika kiti chache cha kifalme, kuishia mwana wa kwanza wa mfungwa aliyekuwa chumbani kifungoni nao wana wote wa kwanza wa nyama wa kufuga. Ndipo, Farao alipoamka usiku, yeye na watumishi wake wote na Wamisri wote, maombolezo yakawa makuu huko Misri, kwani hakuna nyumba isiyokuwa na mfu. Naye akamwita Mose na Haroni usiku, akawaambia: Ondokeni, mtoke katikati yao walio ukoo wangu, ninyi na wana wa Isiraeli! Nendeni kumtumikia Bwana, kama mlivyosema! Nao mbuzi na kondoo na ng'ombe wenu wachukueni, kama mlivyosema! Haya! Nendeni, mnibariki nami! Wamisri nao wakawahimiza hao watu na kuwatoa upesi katika nchi yao, kwani walisema: Sisi sote tutakufa. Watu wakauchukua unga wao uliokandwa, ukiwa haujachachuka bado, nayo mabakuli yao ya kukandia wakayafunga katika nguo zao, wakayachukua mabegani. Nao wana wa Isiraeli walikuwa wameyafanya, Mose aliyowaambia, wakiwatakia Wamisri vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu na nguo. Naye Bwana aliwapatia hawa watu upendeleo machoni pa Wamisri, nao wakawakopesha; hizi ndizo nyara, walizoziteka huko Misri. Hivyo ndivyo, wana wa Isiraeli walivyoondoka Ramusesi kwenda Sukoti, nao walikuwa wanawaume tu waliokwenda kwa miguu 600000 pasipo watoto. Nao wengine wengi waliochanganyika nao wakapanda nao, tena mbuzi na kondoo na ng'ombe, kundi kubwa sana. Nao ule unga uliokandwa, waliouchukua walipotoka Misri, wakauoka kuwa maandazi na mikate isiyochachwa, kwani ulikuwa haukuchachuka, kwani walikimbizwa kutoka Misri, hawakuweza kukawilia wala kutengeneza pamba za njiani. Miaka ya kukaa, wana wa Isiraeli waliyokaa Misri, ilikuwa miaka 430. Hii miaka 430 ilipokwisha pita, siku iyo hiyo vikosi vyote vya Bwana vilitoka katika nchi ya Misri. Usiku huo wa kuwatoa katika nchi ya Misri ulikuwa usiku wa Bwana wa kuangaliwa; kwa hiyo usiku huo wa Bwana na uwe wa kuangaliwa kwa wana wote wa Isiraeli na kwa vizazi vyao vijavyo. Bwana akamwambia Mose na Haroni: Haya ndiyo maongozi ya Pasaka: mtu asiye wa kwenu asiile! Lakini kila mtumwa aliyenunuliwa kwa fedha ataila, ukiisha kumtahiri. Atakayekaa tu kwako na mtu wa mshahara asiile! Sharti iliwe katika kila nyumba, lakini usitoe nyama yake yo yote mle nyumbani na kuipeleka nje, wala msimvunje mfupa wo wote! Wao wote wa mkutano wa Waisiraeli sharti wafanye hivyo. kama mgeni anakaa ugenini kwako, naye akitaka kuila Pasaka ya Bwana, uwatahiri wote walio wa kiume kwake, kisha ataweza kuikaribia kuila, maana atakua kama mzalia wa hiyo nchi, lakini kila asiyetahiriwa asiile! Maonyo yawe yayo hayo ya mzalia wa kwenu nayo ya mgeni atakayekaa ugenini kwako! Nao wana wa Isiraeli wote wakayafanya; kama Bwana alivyomwagiza Mose na Haroni, ndivyo, walivyofanya. Ilikuwa siku ileile moja tu, Bwana akiwatoa wana wa Isiraeli katika nchi ya Misri vikosi kwa vikosi. Bwana akamwambia Mose kwamba: Kila mtoto mume atakayezaliwa wa kwanza na mama yake ye yote, kama ni wa mtu au wa nyama wa kufuga kwao wana wa Isiraeli, sharti amtoe kuwa wangu mimi. Kwani ni wangu kweli. Mose akawaambia hao watu: Ikumbukeni siku hii ya leo kuwa ndiyo, mliyotoka huko Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa! Kwani Bwana amewatoa huko kwa mkono wenye uwezo, siku hiyo kisiliwe cho chote chenye chachu. Siku hii ndiyo, mliyotoka nayo katika mwezi wa Abibu. Napo hapo, Bwana atakapokupeleka katika nchi yao Wakanaani na Wahiti na Waamori na Wahiwi na Wayebusi, aliyowaapia baba zako kukupa wewe, katika ile nchi ichuruzikayo maziwa na asali, huko shari uuangalie utumishi huu, uutumikie katika mwezi huu! Siku saba ule mikate isiyochachwa, nayo siku ya saba iwe ya sikukuu yenyewe! Mikate isiyochachwa iliwe siku saba, isionekane kwako wala mikate iliyochachwa wala chachu yo yote katika mipaka yako! Nao wanao na uwaeleze siku hiyo kwamba: Ni kwa kuwa Bwana alitufanyia haya na haya, tulipotoka kule Misri. Nayo sharti yawe kwako kielekezo mkononi pako na ukumbusho katikati ya macho yako, Maonyo ya Bwana yapate kuwa kinywani mwako, kwani Bwana amekutoa huko Misri kwa mkono wenye uwezo. Nayo maongozi haya sharti uyaangalie, uyafuate, siku zao zitakapotimia mwaka kwa mwaka! Hapo Bwana atakapokuingiza katika nchi ya Kanaani, kama alivyokuapia wewe na baba zako, akakupa, iwe yako, ndipo umtolee Bwana kila atakayezaliwa wa kwanza na mama yake naye kila mwana wa nyama wa kufuga atakayekuwa wa kwanza, utakayempata, wao wa kiume watakuwa wake Bwana. Kila mwana wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana kondoo; usipomkomboa mvunje shingo! Naye kila mwana wa kwanza wa mtu kwao wanao utamkomboa. Tena kama mwanao atakuuliza kesho kwamba: Haya maana yake nini? utamwambia: Bwana alitutoa kwa mkono wenye uwezo kule Misri nyumbani, tulimokuwa watumwa. Farao alipojishupaza, asitupe ruhusa kwenda zetu, Bwana aliwaua wana wote wa kwanza katika nchi ya Misri, wao waliokuwa wana wa kwanza wa watu nao waliokuwa wana wa kwanza wa nyama wa kufuga; kwa hiyo ninamtolea Bwana wana wao wote wanaozaliwa wa kwanza wa mama zao walio wa kiume, nao wana wa kwanza wa wanangu ninawakomboa. Haya na yawe kielekezo mkononi pako, yafungwe napo pajini pako katikati ya macho yako! Kwani Bwana alitutoa Misri kwa uwezo wa mkono wake. Farao alipokwisha kuwapa hawa watu ruhusa kwenda zao, Mungu hakuwashikisha njia ya kupita katika nchi ya wafilisti iliyokuwa fupi, kwani Mungu alisema: Labda watu hawa watageuza miyo kwa kuona vita, warudi Misri. Kwa hiyo Mungu akawazungusha hao watu na kuwashikisha njia ya nyikani kwenye Bahari Nyekundu. Nao wana wa Isiraeli walipotoka katika nchi ya Misri walikuwa wenye mata. Mose akaichukua nayo mifupa ya Yosefu kwenda nayo, kwani yeye aliwaapisha wana wa Isiraeli kwamba: Hapo, Mungu atakapowakagua ninyi, sharti mwichukue mifupa yangu, mwitoe huku kwenda nayo. Walipoondoka Sukoti wakapiga makambi Etamu kwenye mpaka wa hiyo nyika. Naye Bwana akawaongoza akiwatangulia mchana kwa wingu jeusi lililokuwa kama nguzo, awaongoze njia, tena usiku kwa moto uliokuwa kama nguzo, uwamulikie, wapate kwenda mchana na usiku. Ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana mbele yao hao watu, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku mbele yao. Bwana akasema na Mose kwamba: Waambie wana wa Isiraeli, warudi, wapige makambi ya kuelekea Pi-Hahiroti katikati ya Migidoli na baharini; hapo panapoelekea Baali-Sefoni ndipo, mpige makambi karibu ya baharini. Ndipo, Farao atakapowawazia wana wa Isiraeli kwamba: Wao wamekwisha kutatanishwa katika nchi hiyo, nayo nyika imewafungia njia, wasitoke. Nami nitaushupaza moyo wa Farao, ajihimize kuwafuata, nijipatie utukufu kwake Farao na kwa vikosi vyake vyote, Wamisri watambue, ya kuwa mimi ni Bwana. Basi, wakafanya hivyo. Mfalme wa Misri alipopashwa habari, ya kama wale watu wamekimbia, ndipo, moyo wake Farao, nayo mioyo ya watumishi wake ilipogeuka kuwataka tena wale watu, wakasema: Hapo tumefanya nini, tukiwapa Waisiraeli ruhusa kwenda zao na kuziacha kazi za kututumikia sisi? Kisha akalitengeneza gari lake, akawachukua nao watu wake kwenda naye, tena akachukua magari ya vita 600 yaliyochaguliwa na magari yote yaliyopatikana huko Misri, nao wakuu, aliowatia katika kila gari lake. Maana Bwana alikuwa ameushupaza moyo wake Farao, mfalme wa Misri, ajihimize kuwafuata wana wa Isiraeli, ijapo Waisiraeli walitoka kwa nguvu za mkono ulioko juu. Wamisri wakawafuata na kupiga mbio, farasi na magari yote ya Farao na wapanda farasi wake na vikosi vyake, wakawafikia kwenye bahari, walikopiga makambi, huko Pi-Hahiroti kuelekea Baali-Sefoni. Farao alipofika karibu, wana wa Isiraeli wakayainua macho yao, wakawaona Wamisri, walivyofuata nyuma; ndipo, waliposhikwa na woga kabisa, wakampigia Bwana makelele wao wana wa Isiraeli. Naye Mose wakamwambia: Kumbe kule Misri hakuna makaburi, ukituchukua, tujifie huku nyikani? Ni kwa sababu gani ukitufanyizia haya kwa kututoa Misri? Neno hili silo, tulilokuambia huko Misri kwamba: Tuache, tuwatumikie Wamisri? Kwani inatufalia zaidi kuwatumikia Wamisri kuliko kujifia nyikani. Lakini Mose akawaambia hao watu: Msiogope! Jipeni mioyo! Ndipo, mtakapouona wokovu wa Bwana, atakaowapatia leo; kwani hawa Wamisri, mnaowaona leo, hamtawaona tena kale na kale. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza tu. Bwana akamwambia Mose: Unanipigiaje makelele? Waambie wana wa Isiraeli, waondoke! Wewe nawe iinue fimbo yako na kuikunjulia bahari mkono wako, uitenge! Ndivyo, wana wa Isiraeli watakavyopita pakavu katikati ya bahari. Nami utaniona, nikiishupaza mioyo ya Wamisri, waingie nao na kuwafuata ninyi, nijipatie utukufu kwake Farao na kwa vikosi vyake vyote, kwa magari yake na kwao wapanda farasi wake. Wamisri watambue, ya kuwa mimi ni Bwana, nikijipatia utukufu kwake Farao na kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. Kisha malaika wa Mungu aliyekuwa akiwatangulia vikosi vya Waisiraeli akaondoka kwenda nyuma yao, nalo wingu lililokuwa kama nguzo likaondoka mbele yao, likaenda kusimamama nyuma yao, likatua hapo katikati ya makambi ya Wamisri na makambi ya Waisiraeli; huko likawa wingu lenye giza, lakini huku likauangaza usiku; kwa hiyo hawakuweza kukaribiana wale na hao usiku kucha. Mose alipoikunjulia bahari mkono wake, Bwana akaiendesha bahari kwa nguvu ya upepo uliotoka upande wa maawioni kwa jua na kuvuma kabisa usiku wote, akaipwelesha bahari kuwa pakavu, maji yakigawanyika. Ndipo, wana wa Isiraeli walipopaingia pale pakavu katikati ya bahari, maji ya bahari yakawa kama ukuta kuumeni na kushotoni kwao. Wamisri wakawafuata mbiombio, farasi wa Farao na magari yake nao walioyapanda, wote pia wakaingia nyuma yao humo katikati ya bahari. Asubuhi kulipopambazuka, Bwana akavichungulia vikosi vya Wamisri toka lile wingu lenye moto na giza, akavistusha vikosi vya Wamisri akaiondoa magurudumu ya magari yao na kuyarusha kwa nguvu. Ndipo, Wamisri walipoambiana: Na tuwakimbie Waisiraeli! Kwani Bwana anawapigania, sisi Wamisri tushindwe. Lakini Bwana akamwambia Mose: Ikunjulie bahari mkono wako, maji yarudiane na kuwatosa Wamisri na magari yao pamoja nao walioyapanda! Mose alipoikunjulia bahari mkono wake, ndipo, maji ya bahari yalipourudia mwendo wake wa siku zote, nayo yalifanyika, kulipopambazuka. Nao Wamisri walipokimbia wakapatwa nayo; ndivyo, Bwana alivyowakumba Wamisri kuingia katikati ya bahari. Maji yakarudiana na kuyafunikiza magari pamoja nao waliopanda farasi, ndio vikosi vyote vya Farao walioingia baharini na kuwafuata Waisiraeli, hakusalia kwao hata mmoja. Lakini wana wa Isiraeli walipita pakavu katikati ya bahari, maji yakiwasimamia kama ukuta kuumeni na kushotoni kwao. Ndivyo, Bwana alivyowaokoa siku ile mikononi mwao Wamisri, kisha Waisiraeli wakaiona mizoga ya Wamisri ufukoni kwenye bahari. Waisiraeli walipoliona tendo hili kubwa, mkono wa Bwana ulilowafanyizia Wamisri, ndipo, watu hao walipomwogopa Bwana, wakamtegemea Bwana naye mtumishi wake Mose. Hapo ndipo, Mose na wana wana Isiraeli walipomwimbia Bwana wimbo huu, wakasema kwamba: Na nimwimbie Bwana! Kwani ni mtukufu mno, Farasi pamoja nao waliowapanda amewatosa baharini. Bwana ni uwezo wangu na wimbo wangu, hunipatia wokovu. Yeye ni Mungu wangu, kwa hiyo na nimsifu, ni Mungu wa baba yangu, kwa hiyo na nimtukuze! Bwana ni mpiga vita, Bwana ni Jina lake. Magari ya Farao na vikosi vyake amewabwaga baharini, wateule wake wakuu wametoswa katika Bahari Nyekundu; vilindi vikawafunika, wakazama chini kama mawe. Mkono wako wa kuume, Bwana, hutukuka kwa nguvu, unazozifanya, mkono wako wa kuume, Bwana, huwaponda adui. Kwa wingi wa ukuu wako unawaangamiza wao wakuinukiao; ukiyafungua makali yako; huwateketeza kama majani makavu. Kwa kufoka kwa pua yako maji yakakwezwa juu, mawimbi yakasimama, kama yamo chunguni. vilindi vikaganda moyoni mwa bahari. Adui aliposema: Nijihimize kufuata! Nitafika, roho yangu itapata kushiba, nikigawanya nyara; nitauchomoa upanga wangu, mkono wangu uwaangamize: ndipo, ulipouvumisha upepo wako, nayo bahari ikawafunikiza, wakazama kama risasi katika maji makuu. Miongoni mwa miungu yuko nani anayefanana na wewe, Bwana? Yuko nani anayefanana na wewe kwa utukufu na kwa utakatifu? Anayetisha kwa matendo yanayoshangiliwa, naye akifanya vioja? Ulipoukunjua mkono wako wa kuume, nchi ikawameza. Umewaongoza kwa huruma yako hao watu, uliowakomboa, ukawafikisha kwa nguvu zako huko, utukufu wako unakokaa. Makabila ya watu walipovisikia wakatetemeka; uchungu ukawapata wenyeji wa Ufilisti. Ndipo, wakuu wa Edomu walipostuka nao, nao madume wa Moabu wakapigwa bumbuazi, nao wenyeji wa Kanaani wakayeyuka wote. Mastuko na maogofyo yakawaangukia, wakanyamaza kimya kama mawe kwa ukuu wa mkono wako, mpaka wapite wao walio ukoo wako, Bwana, mpaka wapite wao wa ukoo huo, uliowakomboa. Waingize na kuwapanda kwenye milima iliyo fungu lako, ulikotengeneza Kao la kukalia wewe Bwana, ililolisimika mikono yako, Bwana, kuwa Patakatifu. Bwana atakuwa mfalme kale na kale. Kwani farasi wa Farao na magari yake pamoja nao walioyapanda walipoingia baharini, Bwana akayarudisha maji ya bahari juu yao, wana wa Isiraeli walipokwisha kupita pakavu katikati ya bahari. Ndipo, mfumbuaji wa kike Miriamu, umbu lake Haroni, alipochukua patu mkononi mwake, nao wanawake wote wakatoka, wamfuate na kupiga patu na kucheza ngoma. Naye Miriamu akawaitikia kwamba: Mwimbieni Bwana! Kwani ni mtukufu mno, Farasi pamoja nao waliowapanda amewatosa baharini! Kisha Mose akawasafirisha Waisiraeli na kuwaondoa kwenye Bahari Nyekundu, wakatoka hapo, wakaingia katika nyika ya Suri, wakaenda siku tatu pasipo kuona maji. Kisha wakafika Mara, lakini hawakuweza kuyanywa yale maji ya Mara, kwani yalikuwa machungu; kwa hiyo wakapaita mahali pale Mara (Uchungu). Ndipo, watu walipomnung'unikia Mose kwamba: Tunywe nini? Naye alipomlilia Bwana, Bwana akamwonyesha mti; alipoutupa mti huo majini, maji yakawa matamu. Hapo Bwana akawatolea maongozi yapasayo, akawajaribu hapo akiwaambia: Kama utaisikia sauti ya Bwana Mungu wako na kuyafanya yanyokayo machoni pake na kuyategea maagizo yake masiko yako na kuyaangalia maongozi yake yote, ndipo, utakapoona, ya kuwa sikutii yale magonjwa yote, niliyowatia Wamisri, kwani mimi Bwana ni mponya wako. Kisha wakafika Elimu palipokuwa visima vya maji 12 na mitende 70, wakapiga makambi hapo penye maji. Walipoondoka Elimu, wakaingia wao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli katika nyika ya sini iliyoko katikati ya Elimu na Sinai siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili tangu hapo, walipotoka Misri. Huko nyikani wao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli wakamnung'unikia Mose na Haroni, wakawaambia: Afadhali tungalikufa katika nchi ya Misri kwa kupigwa na mkono wa Bwana. Huko tulikaa na masufuria yenye nyama, tukapata vyakula vya kushiba, kwani mmetutoa huko na kutuleta huku nyikani, mwaue kwa njaa wao wote walio wa mkutano huu. Ndipo, Bwana alipomwambia Mose: Mtaniona, nikiwanyeshea ninyi mvua ya mikate toka mbinguni, watu watoke tu kuiokota kila siku iipasayo hiyo siku, nipate kuwajaribu, kama wataendelea kuyashika maonyo yangu, au kama sivyo. Lakini siku ya sita watakapotengeneza, waliyoiingiza, itakuwa ileile mara mbili, waliyoiokota siku zote. Kisha Mose na Haroni wakawaambia wana wote wa Isiraeli: Jioni na mjue, ya kuwa ndiye Bwana aliyewatoa ninyi katika nchi ya Misri. Tena asubuhi na mwuone utukufu wa Bwana, kwani amesikia, mlivyomnung'unikia yeye Bwana; maana sisi tu watu gani, mkitunung'unkia? Tena Mose akawaambia: Mtamjua Bwana hapo, atakapowapa leo jioni nyama za kula, tena asubuhi mikate ya kushiba, kwani Bwana amesikia, mlivyomnung'unikia yeye, maana sisi tu watu gani? Hamkutunung'unikia sisi, ila Bwana. Kisha Mose akamwambia Haroni: Waambie wao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli: Njoni kumtokea Bwana! Kwani ameyasikia manung'uniko yenu. Ikawa, Haroni aliposema nao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli, nao walipogeuka kutazama upande wa nyikani, mara utukufu wa Bwana ukatokea winguni. Kisha Bwana akamwambia Mose kwamba: Nimeyasikia manung'uniko ya wana wa Isireli, sasa waambie kwamba: Saa za jioni mtakula nyama, tena asubuhi mtashiba mkate; ndipo, mtakapotambua, ya kuwa mimi Bwana ni Mungu wenu. Jioni tombo wakaja, wakayafunika makambi, tena asubuhi umande ulikuwa umeanguka kuyazunguka makambi. Napo, umande uliokuwa umeanguka ulipoondoka, wakaona nyikani po pote punje ndogo sana zilizoviringana, nazo zilikuwa kama vitone vidogo vya umande juu ya nchi vilivyogandishwa na baridi. Wana wa Isiraeli walipoviona wakaulizana wao kwa wao: Man huu? ni kwamba: Nini hii? kwani hawakujua, kama ndio nini. Ndipo, Mose alipowaambia: Hiki ndicho kilaji, Bwana alichowapa ninyi kuwa chakula. Nalo hili ndilo neno, Bwana aliloliagiza kwamba: Ziokoteni, kila mtu kama inavyompasa kula, vibaba viwili kwa kichwa kimoja! Sasa chukueni kila mtu kwa hesabu yao, alio nao hemani mwake! Wana wa Isiraeli wakafanya hivyo, wakaokota mmoja nyingi, mmoja chache, lakini walipopima kwa pishi, yule aliyeokota nyingi hakufurikiwa, wala aliyeokota chache hakupungukiwa, ila walikuwa wameokota kila mtu zilizompasa za kula. Kisha Mose akawaambia: Mtu asisaze za kesho! Lakini hawakumsikia Mose, wengine wakasaza za kesho, zikapata funyo ndani, zikanuka vibaya. Naye Mose akawakasirikia. Hivyo wakaokota kila kulipokucha kila mtu zilizompasa za kula; lakini jua lilipowaka na ukali, zikayeyuka. Lakini walipookota siku ya sita, hivyo vilaji vilikuwa kipimo cha siku zote mara mbili, vibaba vinne mtu mmoja. Ndipo, wakuu wote wa mkutano walipokwenda kwa Mose kumpasha habari. Naye akawaambia: Hili ndilo, Bwana alilolisema kwamba: Kesho ni siku takatifu ya mapumziko ya kumpumzikia Bwana. Mnazotaka kuzikaanga zikaangeni! Mnazotaka kuzipika zipikeni! Zitakazosalia jiwekeeni za kungoja kesho! Walipoziweka za kesho, kama Mose alivyowaagiza, kuzikunuka vibaya, wala hazikupata funyo. Mose akawaambia: Zileni leo! Kwani leo ni siku ya mapumziko ya Bwana, leo hamtaziona nje nyikani. Siku sita mtaziokota, lakini siku ya saba ni ya mapumziko, haziko. Wengine walipotoka siku ya saba kuziokota, hawakuziona. Ndipo, Bwana alipomwambia Mose: Mpaka lini mtakataa kuyaangalia maagizo na maonyo yangu? Tazameni: Bwana amewapa ninyi siku ya mapumziko, kwa hiyo huwapa siku ya sita vilaji vya siku mbili. Kaeni tu kila mtu mahali pake, siku ya saba mtu asitoke hapo pake! Kwa sababu hii watu wakapumzika siku ya saba. Wao wa mlango wa Waisiraeli wakaziita jina lake: Mana; nazo zilikuwa nyeupe kama mbegu za mtama mweupe, napo walipozijaribu kula, zikawa tamu kama maandazi yaliyotiwa asali. Mose akasema: Hili ndilo neno, Bwana aliloliagiza: Jaza kisaga cha vibaba viwili mana, kiwekewe vizazi vyenu vijavyo, wapate kuviona vilaji hivi, nilivyowalisha ninyi nyikani nilipowatoa ninyi katika nchi ya Misri. Naye Mose akamwambia Haroni: Chukua kitungi kimoja, ukitie kisaga kimoja cha Mana, kisha kiweke mbele ya Bwana, kiwekewe vizazi vyenu vijavyo! Kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, Haroni alivyokiweka mbele ya Sanduku la Ushahidi, kiangaliwe. Nao wana wa Isiraeli wakala Mana miaka 40, mpaka walipoingia katika nchi iliyokuwa yenye watu; hivyo ndivyo, walivyokula Mana, mpaka walipofika kwenye mipaka ya nchi ya Kanaani. Nacho kile kisaga kilipopimwa kwa mizani kilikuwa fungu la kumi la frasila. Wao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli wakaondoka katika nyika ya sini kwenda safari zao kwa kuagizwa na Bwana, wakapiga makambi Refidimu, lakini maji ya kunywa watu hayakuwako. Ndipo, watu walipomgombeza Mose na kusema: Tupeni maji, tunywe! Mose akawaambia: Mbona mnanigombeza? Mbona mnamjaribu Bwana? Lakini hawa watu kwa kuwa waliona huko kiu ya maji, wakamnung'unikia Mose kwamba: Kwa nini umetutoa kule Misri, utuue kwa kiu sisi na wana wetu na makundi yetu? Naye Mose akamlilia Bwana kwamba: Watu hawa niwafanyie nini? Kidogo tena, wangenipiga mawe. Bwana akamwambia Mose: Pita mbele ya hawa watu, uchukue wazee wengine wa Waisiraeli kwenda pamoja na wewe, nayo ile fimbo yako iliyoupiga ule mto ishike mkononi mwako, kisha nenda! Utakaponiona, nikisimama mbele yako mwambani juu huko Horebu, uupige huo mwamba; ndipo, utakapotoka maji, watu wanywe. Mose akayafanya vivyo hivyo machoni pa wazee wa Kiisiraeli, akapaita Masa na Meriba (Majaribu na Magomvi), kwa kuwa wana wa isiraeli walimgombeza hapo, wakamjaribu naye Bwana wakisema: Je? Bwana yumo katikati yetu au hayumo? Waamaleki wakaja kupigana nao Waisiraeli huko Refidimu. Ndipo, Mose alipomwambia Yosua: Utuchagulie waume, utoke nao kupigana na Waamaleki! Mimi nami nitasimama kesho juu ya hiki kilima, nayo fimbo ya Mungu itakuwa mkononi mwangu. Yosua akafanya, kama Mose alivyomwagiza kwenda kupigana na Waamaleki, lakini Mose na Haroni na Huri wakakipanda hicho kilima, mpaka wafike juu. Ikawa, Mose alipouinua mkono wake, Waisiraeli wakashinda; lakini alipoushusha mkono wake, upumzike, Waamaleki wakashinda. Mikono ya Mose ilipolegea kwa kuwa mizito, wakachukua jiwe, wakaliweka chini yake, apate kulikalia. Kisha Haroni na Huri wakaishikiza mikono yake, mmoja huku, mmoja huko; ndivyo, mikono yake ilivyopata nguvu, mpaka jua lilipokuchwa, tena ndivyo, Yosua alivyowashinda Waamaleki na watu wao kwa ukali wa panga. Bwana akamwambia Mose: Yaandike haya katika kitabu, yakumbukwe siku zote! Tena mwelezee Yosua, ya kama nitafuta kabisa ukumbusho wote wa Waamaleki, watoweke chini ya mbingu. Kisha Mose akajenga pa kumtambikia Bwana, akapaita jina lake: Bwana ni Bendera yangu, kwani alisema: Bwana ameuweka mkono penye bendera kwamba: Bwana atapiga vita na Waamaleki kwa vizazi na vizazi. Yetoro, mtambikaji wa Midiani, aliyekuwa mkwewe Mose, alipoyasikia yote, Mungu aliyomfanyizia Mose nao ukoo wake wa Waisiraeli, ya kuwa Bwana aliwatoa Waisiraeli huko Misri, ndipo, Yetoro, mkwewe Mose, alipomchukua Sipora, mkewe Mose, aliyemrudisha, na wanawe wawili, mmoja jina lake Gersomu (Mgeni wa Huku), kwani alisema: Mimi nimekuwa mgeni katika nchi isiyo ya kwetu; naye wa pili jina lake Eliezeri (Mungu Msaada wangu), kwani alisema: Mungu wa baba yangu amenisaidia, ameniponya upanga wa Farao. Yetoro, mkwewe Mose, alipofika pamoja na wanawe na mkewe kwake Mose huko nyikani, alikokuwa amepanga kwenye mlima wa Mungu, akatuma kumwambia Mose: Mimi mkweo Yetoro nimekuja kwako pamoja na mkeo na wanawe wawili. Ndipo, Mose alipotoka kumwendea njiani, akamwinamia, akanoneana naye, nao wakatakiana kuwa hawajambo, kisha wakaingia hemani. Mose akamsimulia mkwewe yote, Bwana aliyomfanyizia Farao nao Wamisri kwa ajili ya Waisiraeli, nayo masumbuko yote yaliyowapata njiani, tena jinsi Bwana alivyowaponya. Yetoro akayafurahia hayo mema yote, Bwana aliyowafanyizia Waisiraeli na kuwaponya mikononi mwa Wamisri. Kisha Yetoro akasema: Bwana na atukuzwe aliyewaponya mikononi mwa Wamisri namo mkononi mwa Farao, kwa kuwa amewaponya watu hawa na kuwatoa mikononi mwa Wamisri! Sasa ninatambua, ya kuwa Bwana ni mkuu kuliko miungu yote, nao wale walikuwa wamejivunia ukuu wao kwao hawa. Naye Yetoro, mkwewe Mose, akamtolea Mungu ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kuchinjwa, naye Haroni nao wazee wote wa Waisiraeli wakaja kula chakula pamoja na mkwewe Mose mbele ya Mungu. Kesho yake asubuhi Mose akakaa kuwaamua watu, nao watu wakasimama kwake Mose toka asubuhi hata jioni. Mkwewe Mose alipoyaona yote, aliyowafanyia watu, akasema: Hili jambo linakuwaje, ukijisumbua hivyo na hawa watu? Mbona wewe unakaa peke yako, nao hawa watu wanasimama kwako toka asubuhi hata jioni? Naye Mose akamwambia mkwewe: Hawa watu wakija kwangu, ni kwa kuwa wanataka kumwuliza Mungu. Wakipatwa na shauri huja kwangu, niwaamue wao kwa wao na kuwajulisha maongozi ya Mungu na maonyo yake. Naye mkwewe Mose akamwambia: Hivyo, unavyolifanya jambo hili, havifai. Hivyo wewe mwenyewe utalegea kwa uchovu nao watu hao, ulio nao, kwani kazi hii ni ngumu zaidi ya kukushinda, huwezi kuifanya peke yako. Sasa isikie sauti yangu, nikupe shauri, naye Mungu na awe pamoja na wewe! Wewe wasemee watu mbele ya Mungu na kuyapeleka mashauri yao kwake Mungu! Tena uwafundishe maongozi na kuwajulisha njia, watakayoishika, nayo matendo, watakayoyafanya. Lakini tena ujitazamie kwa watu wote wana waume wenye nguvu wamchao Mungu kwa kweli, wachukiao kupenyezewa, wao uwaweke kuwa wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia na wakuu wa hamsini na wakuu wa makumi, wawaamue watu siku zote, kwako walete mashauri makubwa tu, lakini mashauri madogo yote wayakate wao! Hivi mzigo wako utapunguka, wao wakikusaidia kuuchukua. Ukivifanya hivyo, naye Mungu akikuagiza hivyo, wewe utaweza kujitunza, nao watu hawa wote wataweza kwenda zao na kutengemana. Mose akaisikia sauti ya mkwewe, akayafanya yote, aliyoyasema. Kwa hiyo Mose akachagua kwa Waisiraeli wote watu wenye nguvu, akawaweka kuwa vichwa vya watu hawa, maana wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia na wakuu wa hamsini na wakuu wa makumi, wawaamue watu siku zote, lakini mashauri magumu wayalete kwake yeye Mose, lakini mashauri madogo wayakate wao. Kisha Mose akamsindikiza mkwewe, akaenda zake katika nchi yake. Katika mwezi wa tatu tangu hapo, wana wa Isiraeli walipotoka katika nchi ya Misri, siku hiyohiyo wakafika nyikani kwa Sinai. Walipoondoka Refidimu, wakafika nyikani kwa Sinai; nao Waisiraeli wlipoyapiga makambi yao wakayapiga ng'ambo ya huku kwenye huo mlima. Naye Mose akaupanda huo mlima kwenda kwake Mungu, Bwana alipomwita huko mlimani, akamwambia: Hivi ndivyo, utakavyowaambia wao wa mlango wa Yakobo na kuwatangazia wana wa Isiraeli: Ninyi mmeyaona niliyowafanyizia Wamisri, nikawachukua ninyi, kama tai anavyowachukua watoto wake mabawani, nikawafikisha kwangu. Sasa mtakapoisikia sauti yangu na kuliangalia Agano langu, mtakuwa watu wangu mwenyewe kuliko makabila yote ya watu, kwani ulimwengu wote ni wangu. Ninyi mtakuwa ufalme wangu wenye watambikaji na taifa takatifu. Haya ndiyo maneno, utakayowaambia wana wa Isiraeli. Mose aliporudi akawaita wazee wao hawa watu, akawaeleza haya maneno yote, Bwana aliyomwagiza. Watu wote wakaitikia pamoja kwamba: Yote, Bwana aliyoyasema, tutayafanya. Naye Mose akampelekea Bwana majibu haya ya watu; Bwana naye akamwambia Mose: Utaniona mimi, nikikujia katika wingu jeusi, hawa watu wasikie, nikisema na wewe, wakutegemee nawe kale na kale. Kisha Mose akamsimulia Bwana maneno yote ya watu. Kisha Bwana akamwambia Mose: Nenda kwao hawa watu, uwaeue leo na kesho, wazifue nazo nguo zao, wawe tayari siku ya tatu! Kwani hiyo siku ya tatu Bwana atashuka machoni pao watu wote kufika juu ya mlima wa Sinai. Tena uwakatie hawa watu mpaka wa kuuzunguka mlima na kuwaambia: Jiangalieni, msiupande mlima huu, wala msiuguse hapo chini yake! Kwani kila atakayeugusa mlima huu atakufa; lakini mkono wa mwingine usimguse mtu huyo, ila auawe kwa kupigwa mawe au kwa kuchomwa mikuki, kama ni mtu au nyama, asiwepo tena! Lakini hapo, panda lenye mlio mrefu litakapopigwa, ndipo wao nao na waupande mlima huu! Kisha Mose akatelemka huko mlimani kwenda kwao hao watu, akawaeua watu, wakazifua nguo zao. Tena akawaambia: Msiwakaribie wake zenu, mpate kuwa tayari siku ya tatu! Siku ya tatu ilipofika, ilipokuwa asubuhi, zikasikilika ngurumo, nao umeme ukapiga, nako mlimani juu kukawa na wingu jeusi, nao mlio wa baragumu lenye nguvu ukasikilika, nao watu wote waliokuwa makambini wakatetemeka. Ndipo, Mose alipowatoa watu makambini, waje kukutana na Mungu, wakajipanga mlimani chini. Lakini mlima wote wa Sinai ulitoka moshi, kwa kuwa Bwana aliutelemkia kwa moto, nao moshi wake ukapanda, kama moshi wa tanuru, nao mlima wote ukatetemeka sana, nao mlio wa lile baragumu ukaendelea, ukazidi sana. Mose akasema, naye Mungu akamwitikia na kupaza sauti. Bwana alipokwisha kushuka huko kwenye mlima wa sinai na kufika kileleni juu ya mlima huu, Bwana akamwita Mose kufika kileleni juu ya mlima huu, naye Mose akapanda. Ndipo, Bwana alipomwambia Mose: Shuka, uwaonye hawa watu, wasijivunjie njia ya kufika kwa Bwana, wapate kumwona, wasife wengi miongoni mwao. Nao watambikaji watakaomkaribia Bwana, sharti wajieue, Bwana asije, akawaponda. Lakini Mose akamwambia Bwana: Hawa watu hawawezi kupanda mlimani kwa Sinai, kwani wewe mwenyewe umetuonya na kuniagiza kwamba: Kata mpaka wa mlima huu na kuueua, wasiuguse. Ndipo, Bwana alipomwambia: Nenda, ushuke! Kisha upande wewe, naye Haroni pamoja na wewe! Lakini watambikaji na watu wasijivunjie njia ya kupanda kwake Bwana, asije, akawaponda. Kisha Mose akatelemka kwenda kwao hao watu, akawaambia maneno hayo. Mungu akayasema maneno haya yote kwamba: Mimi ndimi Bwana Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa. usiwe na miungu mingine ila mimi! Usijifanyie kinyago wala mfano wo wote wa vitu vilivyoko mbinguni juu, wala vilivyoko nchini chini, wala vilivyomo majini chini ya nchi! Usivitambikie, wala usivitumikie! Kwani mimi Bwana Mungu wako ni Mungu mwenye wivu; manza za baba nitazipatilizia wana, nikifikishe kizazi cha tatu na cha nne, kwao wanichukiao. Lakini nitawafanyizia mema, nikifikishe hata kizazi cha maelfu, kwao wanipendao na kuyashika maagizo yangu. Usilitaje Jina la Bwana Mungu wako bure! Kwani Bwana hatamwachilia alitajaye Jina lake bure. Ikumbuke siku ya mapumziko kuitakasa! Siku sita sharti ufanye kazi, uyamalize mambo yako yote! Lakini siku ya saba ndiyo ya kumpumzikia Bwana Mungu wako. Hapo usifanye kazi yo yote, wala wewe, wala mwanao wa kiume, wala wa kike, wala mtumishi wako wa kiume, wala wa kike, wala nyama wako wa kufuga, wala mgeni wako aliomo malangoni mwako. Kwani siku sita Bwana alizifanya mbingu na nchi na bahari navyo vyote vilivyomo, akapumzika siku ya saba; kwa hiyo Bwana aliibariki siku ya saba, akaitakasa. Mheshimu baba yako na mama yako, siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi, akupayo Bwana Mungu wako! Usiue! Usizini! Usiibe! Usimshuhudie mwenzio uwongo! Usiitamani nyumba ya mwenzio! Usimtamani mke wa mwenzio, wala mtumishi wake wa kiume wala wa kike, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote, mwenzio alicho nacho! Nao watu wote walipoziona zile ngurumo na umeme na mlio wa baragumu nao mlima uliotoka moshi, walipoviona hivi vyote wakakimbia, wakasimama mbali, wakamwambia Mose: Sema wewe na sisi, nasi tutasikia! Lakini Mungu asiseme nasi, tusife. Naye Mose akawaambia: Msiogope! Kwani Mungu amekuja kuwajaribu ninyi, kusudi mwone na macho yenu, anavyoogopesha, mwache kumkosea. Kwa hiyo watu wakasimama mbali, lakini Mose akalikaribia lile wingu jeusi, Mungu alimokuwa. Bwana akamwambia Mose: Hivi ndivyo, uwaambie wana wa Isiraeli: Ninyi mmeona, ya kuwa nimesema nanyi toka mbinguni. Kwa hiyo msifanye vyo vyote kuwa Mungu kama mimi, msijifanyizie miungu ya fedha wala miungu ya dhahabu! Unijengee kwa udongo pa kunitambikia, upate pa kunitolea ng'ombe zako za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukruni za kondoo wako na za ng'ombe wako! Napo po pote, nitakapokukumbusha Jina langu, nitakuja kwako, nikubariki. Nawe utakaponijengea kwa mawe pa kunitambikia, usitumie mawe ya kuchonga. Kwani ukiyapiga tu kwa chuma chako cho chote umekwisha kuyatia uchafu. Tena usitumie ngazi ya kupapandia hapo pa kunitambikia, ni kwamba vyako vyenye soni visifunuliwe hapo pake. Haya ndiyo maamuzi, utakayoyaweka mbele yao: Ukinunua mtumwa wa Kiebureo, sharti atumike miaka sita, lakini katika mwaka wa saba atatoka utumwani pasipo kukombolewa. Kama aliingia kwako peke yake tu, na atoke hivyo peke yake tu; kama aliingia mwenye mkewe, mkewe na atoke utumwani pamoja naye. Kama bwana wake alimpa mwanamke, naye akazaa wana wa kiume na wa kike, yule mwanamke pamoja na watoto wake watakuwa mali ya bwana wao, naye mume atatoka utumwani peke yake. Lakini mtumwa atakaposema: Nampenda bwana wangu na mke wangu na watoto wangu, sitaki kutoka utumwani, bwana wake na amtokeze kwa Mungu na kumfikisha penye mlango au penye mwimo, kisha bwana wake na alitoboe hapo sikio lake kwa shazia; ndipo, atakapokuwa mtumwa wake kale na kale. Mtu akimwuza mwanawe wa kike kuwa kijakazi, hatatoka utumwani, kama waume wanavyotoka. Akiwa mbaya machoni pa bwana wake aliyemtaka wa kulala naye, na amtoe, akombolewe; lakini hana ruhusa ya kumwuza kwa watu wa kabila geni, kwani ni yeye aliyemdanganya. Lakini akimpa mwanawe wa kiume kuwa wa kulala naye, sharti amfanyizie zile haki zipasazo mwanawe wa kike. Akijichukulia mwingine, yule asimkatie wala kitoweo chake wala nguo zake wala ngono zake. Asipompatia hayo mambo matatu, atatoka utumwani bure tu pasipo kulipa fedha. Mtu akimpiga mwenzake, hata afe, hana budi kuuawa kabisa. Lakini kama hakumvizia, ikiwa Mungu amemtia mkononi mwake, nitakuonyesha mahali, atakapopakimbilia. Lakini mtu akimnyatia mwenzake, kusudi apate kumwua kwa kumdanganyadanganya, huyo sharti umtoe hata mezani pangu pa kutambikia, auawe. Atakayempiga baba yake au mama yake sharti auawe kabisa. Naye atakayemwiba mwenziwe, kama amekwisha kumwuza, au kama anaonekana angalimo mikononi mwake, sharti auawe kabisa. Naye atakayemwapiza bba yake na mama yake sharti afe kwa kuuawa. Watu wakigombana, mmoja akimpiga mwenzake jiwe au konde, asife, ila augue tu na kulala kitandani, naye akipata kuinuka tena na kujiendea nje kwa kujiegemeza na mkongojo, basi, yule aliyempiga asipatwe na jambo lo lote, atamlipa tu siku za kukaa bure pasipo kufanya kazi, nayo mauguzi hana budi kuyalipa. Mtu akimpiga fimbo mtumwa wake au kijakazi wake, naye akifa papo hapo, anapomshika kwa mkono wake, sharti alipizwe. Lakini akiwapo baadaye siku moja au mbili, hatalipizwa, kwani ni mali yake yeye. Watu wakigombana, tena hapo wakipiga mwanamke mwenye mimba, nayo mimba yake ikiharibika pasipo kumtia ugonjwa, sharti atozwe fedha, kama mumewe yule mwanamke atakavyomtakia; hana budi kuzitoa zizo hizo, waamuzi watakazomwagiza. Lakini akipata kuumizwa zaidi, sharti umtoze roho kwa roho, jicho ka jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, kuugua kwa kuugua, kidonda kwa kidonda, vilio kwa vilio. Mtu akimpiga mtumwa au kijakazi wake jicho na kuliharibu, sharti ampe ruhusa ya kutoka utumwani kwa kumlipa hilo jicho. Hata akimvunja mtumwa au kijakazi wake jino, sharti ampe ruhusa kutoka utumwani kwa kumlipa jino. Ng'ombe akimkumba mwanamume au mwanamke kwa pembe zake, akifa, sharti huyo ng'ombe auawe kwa kupigwa mawe, nyama zake zisiliwe, lakini mwenye ng'ombe hana neno. Lakini kama huyo ng'ombe alikuwa akikumba watu tangu siku nyingi, naye bwana wake alikuwa ameonywa, lakini hakumwangalia huyo ng'ombe, naye akiua mwanamume au mwanamke, basi, huyo ng'ombe sharti auawe kwa kupigwa mawe, naye bwana wake hana budi kuuawa. Lakini akitozwa fedha tu za kujikomboa, sharti azitoe zote, anazotakiwa, ziwe makombozi ya roho yake. Ng'ombe akikumba mtoto wa kiume au mtoto wa kike kwa pembe zake, sharti ahukumiwe vivyo hivyo. Lakini ng'ombe akikumba mtumwa au kijakazi kwa pembe zake, mwenye ng'ombe sharti amlipe bwana wao fedha 30, naye ng'ombe sharti auawe kwa kupigwa mawe. Mtu akiacha shimo wazi au akichimba shimo pasipo kulifunikiza, kisha ng'ombe au punda akitumbukia humo, mwenye shimo sharti alipe fedha za kumrudishia yule bwana mali zake, kisha nyama aliyekufa atakuwa wake. Ng'ombe wa mtu akimkumba ng'ombe wa mwenzake kwa pembe zake, akafa, basi, watamwuza yule ng'ombe aliye mzima, lakini fedha, watakazozipata, sharti wazigawanye, naye ng'ombe aliyekufa sharti wamgawanye. Lakini kama ilikuwa imejulikana, ya kuwa huyo ng'ombe hukumba kwa pembe zake tangu siku nyingi, naye bwana wake hakumwangalia, sharti alipe ng'ombe aliye mzima mahali pake al iyekufa, kisha huyo ng'ombe aliyekufa atakuwa wake. Mtu akiiba ng'ombe au kondoo, akimchinja au akimwuza, kwa ng'ombe mmoja sharti alipe ng'ombe watano, na kwa kondoo mmoja sharti alipe kondoo wanne. Mwizi akikamatwa papo hapo, anapovunjia nyumba, akipigwa, afe, basi, siko kukora manza za damu. Lakini kama jua lilikuwa limekwisha kucha tangu hapo, mwenye kumwua atakuwa amekora manza za damu. Mwizi hana budi kuyalipa aliyokwiba; akiwa hanayo malipo, na auzwe kwa ajili ya wizi wake. Kama nyama, aliyemwiba, anapatikana mkononi mwake angali mzima, kama ni ng'ombe au punda au kondoo, sharti alipe wawili. Mtu akilisha shamba au mizabibu, akiliacha kundi lake, lijiendee kulisha shambani kwa mwingine, sharti amlipe na kuyatoa mazao ya shamba lake yeye na ya mizabibu yake yeye yaliyo mema. Moto ukitoka kwenye kuchoma miiba, ukala miganda iliyokwisha kufungwa au mabua yenye ngano au shamba lo lote, basi, mwenye kuuwasha huo moto sharti ayalipe yaliyoharibika. Mtu akimpa mwenzake fedha au vyombo, amwekee, navyo vikiibiwa nyumbani mwa mwenzake, mwizi akionekana, sharti avilipe mara mbili. Lakini mwizi asipoonekana, mwenye nyumba na apelekwe kwa Mungu, waone, kama siye mwenyewe aliyevichukua vyombo vya mwenzake kwa mkono wake. Shauri lo lote, mtu atakalomshtakia mwenzake, kama ni la ng'ombe au la punda au la kondoo au la nguo au la cho chote kilichopotea, mmoja akisema, ni mali yake yeye, basi, shauri lao hao wawili lipelekwe kwa Mungu; naye, Mungu atakayemtokeza kuwa mwenye kukosa, sharti amlipe mwenzake mara mbili kilichompotea. Mtu akimpa mwenzake ng'ombe au punda au kondoo au nyama wo wote wa kufuga, amtunzie, naye akafa au akaumia au akachukuliwa, mtu asione, mwenyewe na amwapishe mwenzake, amtaje Bwana kwamba hakuchukua mali ya mwenzake kwa mkono wake, kisha yule, mwenzake hana budi kumwitikia, asilipe. Lakini mwizi akimwiba kwake, sharti amlipe yule mwenyewe. Akiraruliwa na nyama, sharti amlete huyo nyama aliyeraruliwa kuwa ushahidi; basi, hivyo hatamlipa aliyeraruliwa. Mtu akikopa nyama kwa mwenzake, naye huyo nyama akiumia au akifa, bwana wake akiwa hayuko, yule hana budi kumlipa. Kama bwana wake yuko hapo, halipi; kama alimkodisha huyo nyama, malipo yamo katika hizo fedha za kukodisha. Mtu akimdanganya mwanamwali asiyeposwa, alale naye, sharti amlipie mali za ukwe, awe mkewe. Baba yake akikataa kabisa kumpa kuwa mkewe, bsi, atatoa fedha zimpasazo mwanamwali za posa. Mwanamke mlozi usimwache, awepo! Kila atakayelala na nyama sharti auawe kabisa. Mtu atakayetambikia miungu mingine, isipokuwa Bwana peke yake, sharti atiwe mwiko wa kuwapo. Mgeni usimwonee wala usimkorofishe! Kwani nanyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Mjane au mtoto aliyefiwa na wazazi usimtese! Utakapomtesa atanililia mimi, mimi nami nitakisikia vema kilio chake. Ndipo, makali yangu yatakapowaka moto, niwaue ninyi kwa upanga, wake zenu wawe wajane, nao watoto wenu wasiwe na baba tena. Ukiwakopesha fedha watu wa ukoo wangu, wakikaa kwako wenye ukosefu, usiwawie kama wakopeshaji wengine, ni kwamba: Msiwatoze faida kubwa za kukopesha! Ukimtoza mwenzako blanketi lake kuwa rehani, sharti umrudishie, mpaka jua likichwa. Kwani hulitumia la kujifunika, hili peke yake ni nguo yake ya kuufunika mwili wake; asipokuwa nalo atalalia nini? Naye atakaponililia, mimi nitamsikia, kwani mimi ni mwenye huruma. Mungu usimtukane! Wala mtawala ukoo wako usimwambie maovu! Usikawilie kutoa malimbuko ya vilaji vyako vingi na ya vinywaji vyako! Naye mwanao wa kwanza unipe, awe wangu! vivyo hivyo sharti uvifanye hata kwa ng'ombe wako na kwa mbuzi na kondoo wako: wana wao wa kwanza na wakae na mama zao siku saba, siku ya nane uwatoe kunipa mimi! Nanyi sharti mwe watu wangu watakatifu, msile nyama aliyeraruliwa porini, nyama zake sharti mwatupie mbwa. Usivumishe habari za uwongo ukifanya bia na mwovu kuwa shahidi wa kukorofisha wengine. Usiwe upande wao walio wengi, wakitaka kufanya mabaya. Wal shaurini usiwafuate walio wengi, ukimpotoa mwenzako. Wala usimpendelee mnyonge shaurini. Ukikuta ng'ombe wa mchukivu wako au punda wake, akipotea, sharti umrudishe kwake. Ukimwona punda wa mchukivu wako, ya kuwa ameanguka kwa kulemewa na mzigo wake, usiwaache peke yao, ila yaache mambo yako, usaidiane navyo. Usilipotoe shauri la mwenzako aliye mkiwa, akipatwa na neno. Jitenge kabisa nayo yaliyo ya uwongo! Usiue mtu asiyekora manza, aliye mwongofu! Kwani aliye mwovu sitamtokeza kuwa hakukosa. Usitwae mapenyezo! Kwani mapenyezo huyapofusha macho yao waonao, tena huyapotoa maneno ya waongofu. Wageni msiwakorofishe! Kwani wenyewe mnaijua mioyo ya wageni, ilivyo, kwani mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Miaka sita upande mbegu katika nchi yako na kuyavuna mapato yake! Katika mwaka wa saba utaiacha tu, ipate kupumzika na kutulia; wakiwa walio wa ukoo wako na waile, nayo yatakayosalia na wayale nyama wa porini; vivyo hivyo uifanyizie nayo mizabibu yako na michekele yako! Siku sita na uzifanye kazi zako! Lakini siku ya saba sharti upumzike, ng'ombe wako na punda wako wapate kutulia, naye mwana wa kijakazi wako pamoja na mgeni wapate kupumzika. Yote niliyowaambia yaangalieni! Majina ya miungu mingine msiyataje, yasisikiwe vinvywani mwenu! Kila mwaka unifanyizie sikukuu mara tatu! Sikukuu ya Mikate isiyochachwa uiangalie: siku saba ule mikate isiyochachwa, kama nilivyokuagiza, nazo siku zake zilizowekwa ni za mwezi wa Abibu, kwani ndio, uliotoka Misri; lakini wasitokee mbele yangu mikono mitupu! Tena sikukuu ya Mavuno ya malimbuko ya kazi za kupanda shambani; tena mwisho wa mwaka sikukuu ya kukusanya, utakapoyakusanya shambani mapato ya kazi zako. Kila mwaka mara tatu waume wako wote sharti watokee mbele ya Bwana Mungu. Damu za ng'ombe zangu za tambiko usizitoe pamoja na mikate iliyochachwa! Wala mafuta ya sikukuu yangu yasilale usiku kucha! Malimbuko ya kwanza ya shamba lako sharti uyapeleke Nyumbani mwa Bwana Mungu wako! Kitoto cha mbuzi usikipike katika maziwa ya mama yake. Utaniona, nikimtuma malaika wangu, akutangulie na kukuangalia njiani, akufikishe mahali pale, nilipokutengenezea. Jiangalieni hapo, alipo, uisikilize sauti yake, usimchokoze! Kwani hatawaondolea makosa yenu mabaya, nalo Jina langu limo mwake. lakini ukiisikiliza vema sauti yake, uyafanye yote, nitakayoyasema, mimi nitakuwa adui yao adui zako, niwasonge wakusongao. Kwani malaika wangu atakutangulia, akufikishe kwao Waamori na Wahiti na Waperizi na Wakanaani na Wahiwi na Wayebusi, nami nitawatowesha. Usiiangukie miungu yao, wala usiitumikie, wala usiyafanye, wao wanayoyafanya, ila mziangushe na kuzivunja kabisa nguzo zao za kutambikia. Mtumikieni Bwana Mungu wenu! Ndipo, atakapokibariki chakula chako na maji yako, hata magonjwa yote nitayaondoa kwako. Katika nchi yako hatakuwako mwanamke mwenye kuharibu mimba au mgumba, nayo hesabu ya siku zako za kuwapo nitaitimiza yote. Mbele yako nitayatanguliza mastusho yangu ya kuzimiza roho za watu wote, utakaowafikia; hivyo nitafanya adui zako wote wakuonyeshe visogo vyao. Nitatanguliza mavu mbele yako, niwafukuze Wahiwi na Wakanaani na Wahiti mbele yako. Lakini sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja, nchi isiwe mapori matupu, wala nyama wa porini wasiwe wengi, wakakusumbua. Ila nitawafukuza mbele yako kidogo kidogo, hata mtakapokuwa wengi wa kuichukua hiyo nchi, iwe yenu. Nami nitakukatia mipaka kutoka kwenye Bahari kwenda kwenye bahari ya Wafilisti, tena kutoka nyikani kwenda hata kwenye lile jito kubwa, kwani wenyeji wa nchi hiyo nitawatia mikononi mwenu, uwafukuze mbele yako. Lakini usifanye agano wala nao wenyewe, wala na miungu yao! Wasikae katika nchi yako, wasikukoseshe, unikosee mimi; lakini utakapoitumikia miungu yao, itakuwia tanzi. Kisha akamwambia Mose: Panda kwake Bwana, wewe pamoja na Haroni na Nadabu na Abihu, tena wazee 70 wa Waisiraeli, mniangukie mngaliko mbali! Kisha Mose na aende peke yake kufika kwake Bwana, lakini wale watu wengine wasifike karibu, wasipande naye. Mose akaja, akawasimulia hao watu maneno na maamuzi yote ya Bwana; nao watu wote wakaitikia kwa kinywa kimoja wakisema: Maneno yote, Bwana aliyoyasema, tutayafanya. Kisha Mose akayaandika maneno yote ya Bwana, akajidamka asubuhi, napo hapo chini penye huo mlima akajenga pa kutambikia, akapasimamishia nguzo kumi na mbili kwa hesabu ya mashina kumi na mawili ya Waisiraeli. Akatuma vijana wa wana wa Isiraeli, watolee hapo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na kumchinjia Bwana ndama waume kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Mose akachukua nusu ya damu zao, akazitia katika mabakuli, nazo nyingine akazimwagia hapo pa kutambikia. Kisha akakichukua Kitabu cha Agano, akakisoma masikioni pa watu; nao wakaitikia kwamba: Yote, Bwana aliyoyasema, tutayafanya kwa kumtii. Ndipo, Mose alipozichukua zile damu, akawanyunyizia watu akisema: Tazameni! Hizi ni damu za Agano, Bwana alilolifanya nanyi na kuwaambia haya maneno yote. Kisha Mose na Haroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wale wazee 70 wa Waisiraeli wakapanda, wakamwona Mungu wa Isiraeli, napo chini ya miguu yake palikuwa kama mahali palipotengenezwa kwa mawe ya safiro yaangazikayo au kama mbingu zenyeye kwa kutakata kwake. Lakini hawa wateule wa wana wa isiraeli hakuwapatia kibaya cho chote kwa mkono wake, ila walikuwapo vivyo hivyo wakila, wakinywa, ijapo walikuwa wamemwona Mungu. Kisha Bwana akamwambia Mose: Panda mlimani, ufike kwangu kuwa huku! Nami nitakupa mbao za mawe zenye Maonyo na maagizo, niliyoyaandika humo, upate kuwafunza. Ndipo, Mose alipoinuka pamoja na mtumishi wake Yosua, naye Mose akapanda mlimani kufika kwake Mungu. lakini wale wazee aliwaambia: Kaeni hapa, mpaka tutakaporudi kwenu! Tazameni, Haroni na Huri mnao! Mtu akiwa na neno, na aje kwao! Mose alipopanda mlimani, wingu likaufunika huo mlima. Nao utukufu wa Bwana ukaja kukaa juu ya mlima wa sinai, nalo wingu likaufunika siku sita. Siku ya saba akamwita Mose toka winguni. Nao utukufu wa Bwana ukaonekana machoni pao wana wa Isiraeli kuwa kama moto ulao huko juu mlimani. Mose akaingia mle winguni katikati alipoupanda huo mlima. Mose akawa huko mlimani siku 40 mchana kutwa na usiku kucha. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waambie wana wa Isiraeli, wanichangie vipaji vya tambiko, mtoze kila mtu, kama moyo wake unavyomtuma. Navyo vipaji vya tambiko, mtakavyowatoza, ni hivi: dhahabu na fedha na shaba, na nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na nguo za bafta na nywele za mbuzi, na ngozi nyekundu za madume ya kondoo na ngozi za pomboo na migunga, mafuta ya taa, manukato ya kutengeneza mafuta ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri; vito vya oniki na vito vingine vya kutia katika kisibau cha mtambikaji mkuu na katika kibati chake cha kifuani. Wanitengenezee Patakatifu, nipate kukaa katikati yao. Kwa mfano, mimi nitakaokuonyesha wa hilo kao na wa vyombo vyake vyote, mvifanye vyote pia, viwe vivyo hivyo. Tengenezeni sanduku la mbao za migunga, urefu wake uwe mikono miwili na nusu, nao upana wake uwe mkono mmoja na nusu, nao urefu wake wa kwenda juu uwe mkono mmoja na nusu. Ulifunikize lote dhahabu tupu, upande wa ndani na wa nje uufunikize hivyo, kisha uzungushe juu yake taji la dhahabu. Tena utengeneze mapete manne kwa kuyeyusha dhahabu, uyatie penye pembe zake nne, mapete mawili upande wake mmoja, tena mapete mawili upande wake wa pili. Kisha utengeneze mipiko miwili ya migunga, nayo ifunikize dhahabu, kisha hiyo mipiko itie katika yale mapete pande zote mbili za sanduku, iwe ya kulichukulia hilo sanduku. Namo katika hayo mapete ya sanduku mipiko sharti ikae humo, isitoke humo. Namo sandukuni uuweke Ushahidi, nitakaokupa. Kisha utengeneze kifuniko cha dhahabu tupu kuwa Kiti cha Upozi, urefu wake uwe mikono miwili na nusu, nao upana wake uwe mkono mmoja na nusu. Kisha utengeneze Makerubi mawili ya dhahabu, nayo uyatengeneze kwa kuzifuafua hizo dhahabu, uyaweke pande zote mbili za mwisho wa kifuniko. Kerubi moja uweke upande wa mwisho wa huku, nalo la pili upande wa mwisho wa huko. Hivyo myaweke hayo Makerubi pande zake zote mbili za mwisho wa kifuniko. Nayo Mkerubi yawe yameyakunjua mabawa juu, yakifunike hicho kifuniko kwa mabaa yao, nazo nyuso zao ziwe zimeelekeana, hayo Mkerubi yakikitazama kifuniko kwa nyuso zao. Kisha kifuniko kiweke juu ya lile sanduku, namo sandukuni uuweke Ushahidi, nitakaokupa. Mahali hapo ndipo, nitakapokutana na wewe, niseme na wewe nikiwa hapo juu ya hicho Kiti cha Upozi katikati ya hayo Makerubi mawili yaliyoko juu ya Sanduku la Ushahidi, nikuambie yote, nitakayokuagiza ya kuwaambia wana wa Isiraeli. Tena tengeneza meza kwa mbao za migunga, urefu wake uwe mikono miwili, nao upana wake uwe mkono mmoja, nao urefu wake wa kwenda juu uwe mkono mmoja na nusu. Nayo uifunikize dhahabu tupu, kisha uzungushe juu yake taji la dhahabu. Kisha uzungushe kando yake kibao cha kukingia chenye upana wa shibiri, nacho hicho kikingio ukizungushie taji la dhahabu. Kisha itengenezee mapete manne ya dhahabu, nayo hayo mapete uyatie penye pembe zake nne zilizoko penye miguu yake minne. Hayo mapete sharti yawe papo hapo chini ya kikingio, wapate kutia humo mipiko ya kuichukulia hiyo meza. Hiyo mipiko uitengeneze nayo kwa migunga na kuifunikiza dhahabu, itumike ya kuichukulia hiyo meza. Hata vyano vyake na vijiko vyake na vitungi vyake na vikombe vyake vinavyotumikia vinywaji vya tambiko sharti uvitengeneze kwa dhahabu tupu. Napo hapo mezani sharti uweke pasipo kukoma mikate ya kuw usoni pangu. Tena utengeneze kinara cha dhahabu tupu! Hiki kinara na kitengenezwe kwa kufuafua dhahabu, ipate kutoka shina lake na mti wake, navyo vikombe vyake na vifundo vyake na maua yake, vyote pia viwe vimetoka katika dhahabu iyo hiyo moja. Matawi sita na yatoke penye mbavu zake, matawi matatu ya kinara na yatoke penye ubavu mmoja, tena matawi matatu ya kinara na yatoke penye ubavu wa pili. Vikombe vitatu vinavyofanana na maua ya mlozi viwe katika kila tawi moja, yaani vifundo pamoja na maua yao. Vivyo hivyo katika matawi yote sita yanayotoka katika mti wa kinara. Lakini katika mti wa kinara viwe vikombe vinne vinavyofanana na maua ya mlozi, yaani vifundo pamoja na maua yao. Tena kila mahali, matawi mawili yanapotoka katika huo mti wake, chini yake kiwe kifundo kimoja. Viwe vivyo hivyo kila mahali, matawi mawili yanapotoka. Nayo matawi yanayotoka katika kinara yawe sita. Vifundo na matawi yao sharti yote yawe kazi moja iliyoyatokeza yote pamoja kwa kuifuafua dhahabu iyo hiyo moja, nayo yawe dhahabu tupu. Kisha utengeneze taa zake saba, nazo hizo taa zake uziweke juu yake, zipaangaze mahala palipo mbele yake. Nazo koleo zake na makato yake yawe ya dhahabu tupu. Sharti ukitengeneze pamoja na hivi vyombo vyake vyote kwa kipande cha dhahabu chenye uzito wa mizigo miwili. Angalia, uyafanye yote kwa mfano, niliokuonyesha mlimani! Kao lenyewe utalitengeneza kwa mapazia kumi yaliyoshonwa kwa nguo za bafta ngumu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu, nayo yawe yenye mifano ya Makerubi, kama mafundi wa kufuma wanavyojua kuitengeneza, nawe uwafanyishe! Urefu wa pazia moja uwe mikono ishirini na minane, nao upana wake uwe mikono minne; kila pazia moja liwe lenye kipimo hiki kimoja, kiwe cha mapazia yote. Mapazia matano yaungwe kila moja na mwenzake kuwa moja, nayo matano ya pili yaungwe vivyo hivyo kila moja na mwenzake kuwa moja. Kisha ushone vitanzi vya nguo nyeusi za kifalme penye upindo wa nje wa kila pazia moja hapo, litakapoungwa na jingine; vivyo hivyo uvitie napo penye upindo wa nje wwa kila pazia la pili hapo, litakapoungwa nalo la kwanza. sharti ushone vitanzi hamsini katika kila pazia moja upande mmoja, na tena vitanzi hamsini katika upindo wa kila pazia la pili upande huo utakaoungwa na pazia la kwanza, hivyo vitanzi vielekeane kila moja na mwenzake. Kisha ufanye vifungo vya dhahabu hamsini, upate kuyafunga mapazia kila moja na mwenzake kwa hiyo vifungo, kao hilo liwe moja. Kisha ufanye mapazia ya nywele za mbuzi kuwa hema juu ya kao lenyewe. Utengeneze mapazia kumi na moja. Urefu wa kila pazia uwe mikono thelathini, nao upana wa kila pazia moja moja uwe mikono minne; hiki kipimo kimoja kiwe chao mapazia yote kumi na moja. Kisha uyaunge mapazia matano kuwa moja, nayo yale sita uyaunge kuwa moja, ukilikunja hilo pazia la sita kuwili hapo mbele ya hema. Kisha ushone vitanzi hamsini katika upande wa nje wa kila pazia moja hapo, litakapoungwa na jingine; vivyo hivyo uvitie napo penye upindo wa nje wa kila pazia la pili hapo, litakapoungwa nalo la kwanza. Kisha ufanye vifungo vya shaba hamsini, hivyo vifungo uvitie katika vitanzi, upate kuliunga hilo hema, liwe moja. Nacho kipande kitakachozidi cha mapazia ya hema cha kuangukia pembeni, hiyo nusu ya pazia itakayoangukia pembeni na iangukie upande wa nyuma wa kao. Nao urefu wa mapazia ya hema utakaozidi ndio mkono mmoja huku na huko, basi, huo mkono na uangukie kila upande wa kao wa kulikingia pembeni. Kisha sharti utengeneze chandalua cha hema kwa ngozi nyekundu za madume ya kondoo, tena utengeneze chandalua cha pili kwa ngozi za pomboo kuwa juu yake. Tena utengeneze mbao za kao lenyewe za migunga, nazo zisimame. Urefu wa kila ubao uwe mikono kumi, nao upana wake kila ubao mmoja uwe mkono mmoja na nusu. Kila ubao mmoja uwe na vigerezi viwili, navyo vitazamane kila kimoja na mwenzake. Vivyo hivyo uvitengenezee kila ubao mmoja wa kao lenyewe. Hizo mbao za kao lenyewe uzitengeneze kuwa ishirini upande wa kusini, ndio upande wa juani. Tena chini ya hizi mbao ishirini utengeneze viguu vya fedha arobaini, viwe viguu viwili chini ya kila ubao mmoja viguu viwili vya kivitilia vigerezi vyake viwili. Hata upande wa pili wa kao, ndio upande wa kaskazini vilevile mbao ishirini na viguu arobaini vya fedha, viguu viwili chini ya kila ubao mmoja, vivyo hivyo viwili chini ya kila ubao mmoja. Lakini upande wa nyuma wa kao unaoelekea baharini uutengenezee mbao sita. Tena utengeneze mbao mbili za pembeni mle kaoni upande wa nyuma. Nazo ziwe kama pacha, toka chini viendelee pamoja zote nzima mpaka juu penye pete la kwanza. Hivi ndivyo, zitakavyokuwa mbao zote mbili za hizo pembe mbili za nyuma. Hivyo zote pamoja zitakuwa mbao nane, navyo viguu vya fedha vitakuwa kumi na sita, viguu viwili chini ya kila ubao mmoja, viwe viguu viwili chini ya kila ubao mmoja. Kisha utengeneze misunguo ya migunga, mitano ya mbao za upande mmoja wa kao, tena misunguo mitano ya mbao za upande wa pili wa kao, tena misunguo mitano ya upande wa nyuma wa kao unaoelekea baharini. Nao msunguo wa katikati ulio katikati ya mbao uupitishe toka mwisho wa huku hata mwisho wa huko. Nazo mbao uzifunikize dhahabu, nayo mapete yao uyatengeneze kwa dhahabu, yawe ya kutilia misunguo, nayo misunguo uifunikize dhahabu. Kisha ulisimamishe hilo kao, liwe kama mfano ule ulioonyeshwa mlimani. Tena utengeneze pazia lililoshonwa kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu. Fundi wa kufuma na alitengeneze kuwa lenye mifano ya Makerubi. Kisha ulitungike juu penye nguzo nne za migunga zilizofunikizwa dhahabu, tena ziwe zenye vifungo vya dhahabu, chini ziwe zimesimikwa katika miguu minne ya fedha. Hili pazia ulitungike chini ya hivyo vifungo, kisha uliingize Sanduku la Ushahidi mbele yake pazia, hilo pazia liwatengee Patakatifu na Patakatifu Penyewe. Kisha ukiweke kile kifuniko (Kiti cha Upozi) juu ya Sanduku la Ushahidi pale Patakatifu Penyewe. Nayo ile meza iweke upande wa huku wa pazia, na kinara kile kiweke kuilekea meza upande wa kusini wa kao, lakini meza uiweke upande wa kaskazini. Kisha hapo pa kuingia hemani uweke guo kubwa lililotengenezwa kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu, lifumwe nao wanaojua kweli kufuma kwa nyuzi za rangi. Guo hilo ulitengenezee nguzo tano za migunga, nazo uzifunikize dhahabu, uzitie vifungo vya dhahabu, kisha uzitengenezee miguu ya shaba mitano kwa kuyeyusha shaba. Kisha tengeneza meza ya kutambikia kwa mbao za migunga! Urefu wake uwe mikono mitano, nao upana wake uwe mikono mitano, hiyo meza iwe sawa pande zote nne, nao urefu wake wa kwenda juu uwe mikono mitatu. Pembe zake zinazoipasa uzitie penye pembe zake nne, nazo hizi pembe zake ziwe za mti huohuo mmoja. Kisha hiyo meza uifunikize shaba. Navyo vyombo vyake vya kuondolea majivu na majembe yake na vyano vyake na nyuma zake na sinia zake, vyombo vyake vyote pia uvitengeneze kwa shaba. Kisha utengeneze kikingio kinachofanana na wavu wa shaba, uweke hata mapete manne ya shaba juu ya huo wavu penye pembe zake nne. Huu wavu uuweke chini ya ukingo wa meza ya kutambikia kuelekea chini, huu wavu ufike hapo mpaka katikati ya meza ya kutambikia. Kisha meza ya kutambikia ifanyizie mipiko, hii mipiko iwe ya migunga, nayo uifunikize shaba. Kisha mipiko itiwe katika mapete, hii mipiko iwe pande mbili za meza ya kutambikia, wakiichukua. Uitengeneze kwa mbao, iwe yenye mvungu ndani ulio wazi; kama alivyokuonyesha mlimani, ndivyo waifanye. Kisha utengeneze ua wa hilo kao upande wa kusini ulio wa juani, nguo za huo ua zitengenezwe kwa bafta ngumu, nao urefu wa upande mmoja uwe mikono mia. Nguzo zake ishirini ziwe zenye miguu yao ishirini ya shaba; vifungo vya nguzo na vijiti vyao vya kuziungia juu viwe vya fedha. Hata upande wa kaskazini viwe vivyo hivyo: nguo ziwe zenye urefu wa mikono mia, nazo nguzo zao ishirini ziwe zenye miguu yao ishirini ya shaba, navyo vifungo vya nguzo na vijiti vyao vya kuziungia juu viwe vya fedha. Nao upande wa ua unaoelekea baharini uwe wenye nguo ya mikono hamsini na nguzo zake ziwe kumi zenye miguu yao ya shaba kumi. Nao upana wa upande wa maawioni kwa jua uwe mikono hamsini. Nguo yake upande wa huku iwe ya mikono kumi na mitano, nazo nguzo zake ziwe tatu zenye miguu ya shaba mitatu. Nao upande wa huko nguo yake iwe ya mikono kumi na mitano, nazo nguzo zake ziwe tatu zenye miguu yao ya shaba mitatu. Hapo kati liwe lango la ua lenye pazia la mikono ishirini lililotengenezwa kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu, lifumwe nao wanaojua kufuma kwa nyuzi za rangi. Nguzo zake ziwe nne zenye miguu minne. Nguzo zote zinazouzunguka ua ziwe zimeungwa kwa vijiti vya fedha, navyo vifungo vyao viwe vya fedha, lakini miguu yao iwe ya shaba. Urefu wa ua uwe mikono mia, nao upana mikono hamsini, nao urefu wa kwenda juu mikono mitano. Nguo yake iwe ya bafta ngumu, nayo miguu yake iwe ya shaba. Navyo vyombo vyote vya hili kao vinavyotumika kwa kazi yo yote na mambo zake zote nazo mambo za ua ziwe za shaba. Kisha wewe uwaagize wana wa Isiraeli, wakupatie mafuta ya chekele yaliyotwangwa vema kuwa safi ya kinara ya kutia siku zote katika taa zake. Katika Hema la Mkutanao hapo nje ya pazia lililoko penye Sanduku la Ushahidi Haroni na wanawe wazitengeneze hizo taa, ziwake tangu jioni hata asubuhi mbele ya Bwana pasipo kukoma. Maongozi haya na yawe ya kale na kale kwa vizazi vyao kwa wana wa Isiraeli. Wewe mchukue kaka yako Haroni pamoja na wanawe, uwafikishe kwako ukiwatoa katikati ya wana wa Isiraeli kuwa watambikaji wangu, yeye Haroni na Nadabu na Abihu na Elazari na Itamari, wanawe Haroni. Umtengenezee kaka yako Haroni mavazi matakatifu ya kumpatia macheo na utukufu. Wewe sema nao walio werevu wa kweli mioyoni mwao, niliowapa roho yenye werevu mwingi ulio wa kweli, wamtengenezee Haroni mavazi ya kumweulia, apate kuwa mtambikaji wangu. Nayo mavazi, watakayomfanyizia, ni haya: kibati cha kifuani na kisibau na kanzu na shati ya nguo ya kunguru na kilemba na mshipi. Haya mavazi matakatifu na wamtengenezee kaka yako Haroni, hata wanawe, wawe watambikaji wangu. Nao wale mafundi na watumie nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na nguo za bafta. Kwa kukitengeneza kisibau na watumie dhahabu na nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na nguo za bafta ngumu, kiwe kazi ya ufundi wa kweli. Kiwe chenye vipande viwili vinavyounganika mabegani, penye ncha zake mbili ndipo kifungike. Nayo masombo yake ya kukifunga kifuani pake yawe ya kazi iyo hiyo. Yatengenezwe kwa dhahabu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu. Kisha uchukue vito viwili vya oniki, uchore humo majina ya wana wa Isiraeli. Majina yao sita katika kito kimoja, nayo yale majina sita yaliyosalia katika kito cha pili, kama walivyofuatana kuzaliwa. Kazi hii ya kuchora katika kito na uifanyishe mafundi wanaojua kuchora muhuri. Ndivyo, utakavyoyachora majina ya wanawe Isiraeli katika hivyo vito viwili; kisha uvizungushie vikingo vya dhahabu vya kuvishika. Kisha hivi vito viwili utavibandika penye vile vipande viwili vya mabegani vya kisibau kuwa vito vya kumkumbushia wana wa Isiraeli; hivyo ndivyo, Haroni atakavyoyachukua majina yao juu ya mabega yake mawili mbele ya Bwana, ayakumbuke. Kisha utengeneze nguo zilizofumwa kwa nyuzi za dhahabu tu. Tena tengeneza vikufu viwili vya dhahabu tupu vinavyofanana na kamba nyembamba kwa kuwa kama kamba zilizosokotwa. Kisha hivi vikufu vinavyofanana na kamba uvitie penye zile nguo zilizofumwa kwa nyuzi za dhahabu tu. Kisha kitengeneze kibati cha maamuzi cha kifuani, nacho kiwe kazi ya ufundi wa kweli. Ukitengeneze kuwa kazi nzuri kama ile ya kisibau, ukitumia kwa kukitengeneza dhahabu na nguo za kifame nyeusi na nyekundu na nguo za bafta ngumu. Pande zake zote ziwe sawasawa, tena kiwe kimekunjwa kuwa kuwili, urefu wake uwe shibiri, nao upana, wake uwe shibiri. Ukijaze vito na kuviweka kuwa mistari minne ya vito ya kukijaza chote. Mstari wa kwanza: sardio, topazio na sumarato, ndio mstari wa kwanza. Mstari wa pili: almasi nyekundu, safiro na yaspi; mstari wa tatu: hiakinto, akate na ametisto; mstari wa nne: krisolito, oniki na berilo. Vitakapotiwa viwe vimezungushiwa vyote vikingo vya dhahabu vya kuvishika. Kwa hesabu ya majina ya wanawe Isiraeli viwe kumi na viwili vikiyafuata hayo majina yao, kila kimoja chao kipate jina lake moja katika hayo mashina kumi na mawili, likichorwa humo, kama kazi ya muhuri ilivyo. Tena utengeneze kwa dhahabu tupu vikufu vinavyofanana na kamba zilizosokotwa vya kutia penye kibati cha kifuani. Kisha utengeneze pete mbili kwa dhahabu za kutia penye kibati cha kifuani, kisha uzitie hizo pete mbili penye zile ncha mbili za juu za kibati cha kifuani. Kisha hivyo vikufu vya dhahabu vinavyofanana na kamba uvifunge katika hizo pete mbili, ulizozitia katika ncha za juu za kibati cha kifuani. Kisha hiyo miisho mingine miwili ya hivi vikufu viwili vinavyofanana na kamba uifunge katika vile vikingo viwili vya dhahabu, kisha uvifunge penye vipande vya mabegani vya kisibau upande wake wa mbele. Kisha utengeneze tena pete mbili za dhahabu, uzitie penye zile ncha mbili za chini za kibati cha kifuani katika ukingo wake ulioko upande wa ndani unaokielekea kisibau. Kisha utengeneze tena pete mbili za dhahabu, uzitie katika vipande vile viwili vya mabegani vya kisibau chini upande wake wa mbele papo hapo, vile vipande vinapounganika, juu ya masombo ya kisibau. Kisha na wakifunge kibati cha kifuani kwa kamba ya nguo nyeusi ya kifalme, wakiitia katika pete zake, tena katika pete za kisibau, kibati cha kifuani kipate kukaa juu ya masombo ya kisibau, kisiweze kusogeasogea hapo pake penye kisibau. Hivyo ndivyo, Haroni atakavyoyachukua majina ya wanawe Isiraeli katika kibati cha maamuzi cha kifuani juu ya moyo wake atakapoingia Patakatifu, yakumbukwe usoni pa Bwana siku zote. Tena utie katika kibati cha maamuzi cha kifuani Urimu na Tumimu (Mwanga na Kweli), ziwe juu ya moyo wake Haroni, atakapotokea usoni pa Bwana. Ndivyo, Haroni atakavyoyachukua maamuzi ya wana wa Isiraeli juu ya moyo wake usoni pa Bwana. Kanzu ikipasayo hicho kisibau uitengeneze yote nzima kwa nguo nyeusi ya kifalme. Upande wake wa kichwani iwe na tundu katikati; hili tundu lizungukwe na taraza iliyotengenezwa na mfuma nguo; hili tundu lake liwe kama tundu la shati ya chuma ya mpiga vita, isipasuke. Penye upindo wake wa chini utatia komamanga za nguo za kifalme nyeusi na nyekundu kuuzunguka upindo wake wa chini po pote, tena katikati yao utie po pote vikengele vidogo vya dhahabu, viwe hivyo: kikengele cha dhahabu na komamanga, tena kikengele cha dhahabu na komamanga, vivyo hivyo po pote kuuzunguka upindo wote wa chini wa kanzu. Naye Haroni sharti aivae akitumika, milio yake isikilike, akiingia Patakatifu kutokea usoni pa Bwana, hata akitoka, asife. Kisha utengeneze bamba la dhahabu tupu la pajini, uchore humo kuwa ama machoro ya muhuri: Mtakatifu wa Bwana! Ulifunge kwa kamba ya nguo nyeusi ya kifalme katika kilemba, kiwe mbele ya kilemba. Na kiwe juu ya paji la Haroni, yeye Haroni azichukue manza, wana wa Isiraeli watakazozikora kwa ajili ya vipaji vyao vitakatifu, watakavyomtolea Mungu kuwa vipaji vyao vitakatifu. Na liwe juu ya paji lake siku zote kuwapatia upendeleo machoni pa Bwana. Tena na ufume shati ya bafta kuwa kama nguo ya kunguru, tena utengeneze kilemba cha nguo ya bafta, utengeneze nao mshipi, uwe kazi ya fundi ajuaye kufuma kwa nyuzi za rangi. Nao wana wa Haroni uwatengenezee shati, tena uwatengenezee mishipi, tena uwatengenezee vilemba virefu kuwapatia macheo na utukufu. Kisha umvike kaka yako Haroni mavazi hayo, hata wanawe, uwapake mafuta pamoja na kuwajaza magao yao, ukiwaeua, wapate kuwa watambikaji wangu. Watengenezee nazo suruali nyeupe za ukonge za kuzifunika nyama za miili zitiazo soni, zikitoka viunoni na kufika magotini. Haroni na wanawe sharti wazivae wakiingia katika Hema la Mkutano au wakiikaribia meza ya kutambikia pale Patakatifu, wasife kwa kukora manza. Maongozi haya yawe ya kale na kale kwake nako kwao wa uzao wake wajao nyuma yake. Hili ndilo jambo, utakalowafanyia, uwaeue kuwa watambikaji wangu: chukua dume la ng'ombe aliye kijana bado na madume mawili ya kondoo wasio na kilema, na mikate isiyochachwa na maandazi yasiyochachwa yaliyotiwa mafuta na maandazi membamba yasiyochachwa, yaliyopakwa mafuta juu tu; haya yote uyatengeneze kwa unga mwembamba wa ngano. Kisha yote uyatie katika kikapu kimoja, uyapeleke humo kikapuni pamoja na yule dume la ng'ombe na wale madume mawili ya kondoo. Kisha umfikishe Haroni pamoja na wanawe hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, uwaoshe kwa maji. Kisha yachukue hayo mavazi, umvike Haroni shati na kanzu na kisibau na kibati cha kifuani, kisha umfunge kisibau kwa masombo ya kisibau. Kisha umvike kilemba kichwani pake na kulitia lile bamba takatifu katika kilemba chake. Kisha chukua mafuta ya kumpaka, umpake na kuyamimina kichwani pake. Kisha nao wanawe uwafikishe, uwavike shati; kisha uwafunge mishipi, yeye Haroni na wanawe, uwafunge vilemba virefu; ndipo, utambikaji utakapokuwa wao kwa hayo maongozi ya kale na kale. Kisha umjaze Haroni gao lake, nao wanawe uwajaze magao yao. Kisha umlete dume la ng'ombe, afike hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano; ndipo Haroni na wanawe wambandikie huyo dume la ng'ombe mikono yao kichwani pake. Kisha umchinje huyo dume la ng'ombe mbele ya Bwana hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Kisha uchukue damu kidogo ya huyo dume la ng'ombe, uzipake pembe za meza ya kutambikia kwa kidole chako, nayo damu yote nyingine umwagie msingi wa meza ya kutambikia. Kisha yachukue mafuta yote yanayoufunika utumbo na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo yake mawili nayo mafuta yanayoshikamana nayo, uyachome moto hapo mezani pa kutambikia. Lakini nyama zake huyo dume la ng'ombe na ngozi yake na mavi yake uyateketeze kwa moto nje ya makambi, maana ni ng'ombe ya tambiko ya weuo. Kisha wale madume ya kondoo chukua mmoja, naye Haroni na wanawe na wambandikie huyo dume la kondoo mikono yao kichwani pake Kisha umchinje huyo dume la kondoo, nayo damu yake ichukue, uinyunyizie meza ya kutambikia pande zote. Kisha huyo dume la kondoo umchangue kuwa vipande viwili, kisha uuoshe utumbo wake na miguu yake, upate kuviweka juu y vile vipande vyake na juu ya kichwa chake. Huyo dume la kondoo wote umchome moto hapo mezani pa kutambikia kuwa ng'ombe ya tambiko ya Bwana ya kuteketezwa nzima, ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Kisha mchukue yule dume la kondoo wa pili, naye Haroni na wanawe na wambadikie huyo dume la kondoo mikono yao kichwani pake. Kisha umchinje huyo dume la kondoo, uchukue damu yake kidogo, uwapake Haroni na wanawe pembe za chini za masikio yao ya kuume na vidole gumba vya mikono yao ya kuume na vidole gumba vya miguu yao ya kuume, nayo damu nyingine uinyunyizie meza ya kutambikia pande zote. Kisha uchukue damu kidogo iliyoko mezani pa kutambikia na mafuta ya kupaka kidogo umnyunyizie Haroni na mavazi yake, kisha uwanyunyizie nao wanawe na mavazi ya wanawe; ndivyo, anavyoeuliwa yeye pamoja na mavazi yake, tena ndivyo, nao wanawe wanavyoeuliwa pamoja na mavazi yao. Kisha uyachukue mafuta ya huyo dume la kondoo ni mkia na mafuta yaliyoufunika utumbo na kile kipande cha ini na mafigo yake mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo na paja la kuume, maana ni dume la kondoo apasaye siku ya kujazwa gao. Uchukue tena katika kikapu cha mikate isiyochachwa kilichowekwa mbele ya Bwana mkate mmoja na andazi moja lililotiwa mafuta na andazi jembamba moja. Haya yote uyaweke mikononi mwa Haroni namo mikononi mwa wanawe, uyapitishe motoni mbele ya Bwana. Kisha uyachukue mikoni mwao uyachome moto mezani pa kutambikia kuwa moshi juu ya ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa, hivyo yatakuwa mbele ya Bwana mnuko wa moto wa kumpendeza Bwana. Kisha uchukue kidari cha dume la kondoo la Haroni la kulijaza gao lake, ukipitishe mbele ya Bwana; kisha kitakuwa fungu lako. Ndivyo, utakavyokitakasa kidari kuwa kipaji cha tambiko cha kupitishwa motoni, hata paja kuwa kipaji cha tambiko cha kunyanyuliwa, maana kidari kilipitishwa motoni, nalo paja lilinyanyuliwa kuwa lake Bwana; nacho hicho kidari pamoja na hilo paja yalitoka kwa dume la kondoo wa Haroni na wa wanawe aliyetolewa kuyajaza magao yao. Hii na iwe haki yao Haroni na wanawe ya kale na kale kuyapata kwa wana wa Isiraeli, kwani ndio vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa, na viwe vyao, wana wa Isiraeli watakapotoa ng'ombe za tambiko za shukrani, maana vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa ni vyake Bwana. Nayo mavazi matakatifu ya Haroni na yawe ya wwanawe, watakapomfuata, wayavae watakapopakwa mafuta ya kujazwa magao yao. Mwanawe atakayepata utambikaji sharti ayavae siku saba, apate kuingia katika Hema la Mkutano na kutumikia Patakatifu. Lakini huyo dume la kondoo aliyetolewa kuwajaza magao sharti umchukue, uzitokose nyama zake mahali patakatifu. Naye Haroni na wanawe na wazile nyama zake huyu dume la kondoo pamoja na mikate iliyomo katika kikapu hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Na wazile, kwa kuwa ndizo, walizopatiwa upozi nazo, wapate kujazwa magao pamoja na kueuliwa; lakini mgeni hana ruhusa kuzila, kwani ni takatifu. Kama ziko nyama zitakazosalia zilizokuwa za kuwajaza magao, au kama iko mikate itakayosalia mpaka kesho, sharti uyateketeze hayo masao kwa moto, yasiliwe na mtu, kwani ni matakatifu nayo. Sharti uwafanyizie Haroni na wanawe hivyo vyote, nilivyokuagiza, ukiwajaza magao yao siku saba. Kila siku utatoa dume la ng'ombe aliye kijana bado kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo kumpatia upozi, uieue nayo meza ya kutambikia kwa kuwapatia upozi hapo; kisha umpake mafuta ya kumfanya kuwa mtakatifu. Siku saba nayo meza ya kutambikia uipatie upozi na kuitakasa, ndipo, meza ya kutambikia itakapokuwa takatifu yenyewe, naye kila atakayeigusa sharti awe ametolewa kuwa mtakatifu. Nayo haya ndiyo, utolee mezani pa kutambikia: wana kondoo wawili wa mwaka mmoja kila siku pasipo kukoma. Mwana kondoo mmoja umtoe asubuhi, naye mwana kondoo wa pili umtoe saa za jioni. Tena pamoja na kila mwana kondoo utoe vibaba vitatu vya unga mwembamba uliochanganywa na kibaba kimoja cha mafuta yaliyotwangwa vema, tena kibaba kimoja cha mvinyo kuwa kinywaji cha tambiko. Naye mwana kondoo wa pili na umtoe saa za jioni pamoja na kilaji cha tambiko kama asubuhi; huo utakuwa moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Hizi na ziwe ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, wao wa vizazi vyenu watakazozitoa siku zote mbele ya Bwana hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano; hapo ndipo, nitakapokutana nanyi, napo ndipo, nitakaposema na wewe. Hapo ndipo, nitakapokutana kweli na wana wa Isiraeli, nalo Hema litapata kuwa takatifu kwa ajili ya utukufu wangu. Mimi nitalitakasa Hema la Mkutano na meza ya kutambikia, naye Haroni na wanawe nitawatakasa, wapate kuwa watambikaji wangu. Nami nitakaa katikati ya wana wa Isiraeli, niwe Mungu wao. Nao watajua, ya kuwa mimi Bwana ni Mungu wao aliyewatoa katika nchi ya Misri, nikae katikati yao, mimi Bwana niliye Mungu wao. Tengeneza nayo meza ya kuvukizia mavukizo, uitengeneze nayo kwa migunga. Urefu wake uwe mkono mmoja, nao upana wake uwe mkono mmoja, pande zote nne ziwe sawa, nao urefu wake wa kwenda juu uwe mikono miwili. Uifunikize dhahabu tupu juu yake na kando yake pande zote na pembe zake, kisha uzungushe juu yake taji la dhahabu pande zote. Kisha uitengenezee mapete mawili ya dhahabu, uyatie chini ya taji pande zake mbili penye mbavu zake mbili, yawe ya kutilia mipiko ya kuichukulia. Nayo mipiko uitengeneze kwa migunga, kisha nayo uifunikize dhahabu. Kisha uiweke upande wa huku wa pazia linaloning'inia na kulielekea Sanduku la ushahidi, mbele ya kiti cha upozi kilichoko juu yake Sanduku la Ushahidi nitakapokutana na wewe. Naye Haroni na avukize juu yake mavukizo yanukayo vizuri; kila kunapokucha akizitengeneza taa za kinara na ayavukize. Hata Haroni atakapoziwasha hizo taa saa za jioni na ayavukize tena, mavukizo yavukizwe mbele ya Bwana siku zote nao walio wa vizazi vyenu. Msivukize juu yake manukato mageni, wala msitoe juu yake ng'ombe za tambiko za kuteketezwa wala kipaji cha tambiko. Kila mwaka mara moja Haroni na azipatie upozi pembe zake kwa damu ya ng'ombe ya tambiko ya weuo; mara moja tu kila mwaka na aipatie upozi kwao walio wa vizazi vyenu, maana ni takatifu yenyewe kwa kuwa yake Bwana. Bwana akamwambia Mose kwamba: Ukivihesabu vichwa vyao wana wa Isiraeli, watakapokaguliwa, na wamtolee Bwana makombozi ya kuzikomboa roho zao, kila mtu yake kwa kukaguliwa, wasipatwe na pigo lo lote kwa kukaguliwa. Kwa hiyo kila atakayefika kukaguliwa sharti atoe nusu ya sekeli, ndio fedha zitumikazo Patakatifu, ambazo sekeli moja ni gera ishirini, ndio fedha moja ya thumuni nane. Nusu ya fedha hiyo iwe kipaji cha tambiko cha kumnyanyulia Bwana. Kila atakayefika kukaguliwa mwenye miaka ishirini na zaidi sharti mnyanyulie Bwana hicho kipaji cha tambiko. Mwenye mali asilipe zaidi, wala mnyonge asiipunguze hiyo nusu ya fedha kuwa kipaji cha tambiko cha kumnyanyulia Bwana, wajipatie upozi. Kisha uzichukue hizo fedha za mapoza, utakazowatoza wana wa Isiraeli, uzitumie za utumishi wa hema la Mkutano; ndivyo, zitakavyokuwa za kumkumbusha Bwana, awakumbuke wana wa Isiraeli, azipatie roho zenu upozi. Bwana akamwambia Mose kwamba: Tengeneza birika la shaba lenye wekeo lake la shaba, liwe la kuogea, uliweke katikati ya Hema la Mkutano na meza ya kutambikia, kisha ulitie maji. Haroni na wanawe waoshe humo mikono na miguu yao. Watakapoingia katika Hema la Mkutano wajiogeshe majini, wasife! Au watakapoikaribia meza ya Bwana, watumikie hapo na kumchomea Bwana ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa, na waioshe mikono na miguu yao, wasife! Maongozi haya na yawe ya kale na kale kwake na kwa wazao wake na kwa vizazi vyao. Bwana akamwambia Mose kwamba: Jichukulie manukato yaliyo mazuri mno: manemane mabichi sekeli 500, ndio ratli 20, tena nusu yao dalasini zinukazo vizuri sekeli 250, ndio ratli 10, tena vichiri vinukavyo vizuri sekeli 250, ndio ratli 10, na karafuu sekeli 500, ndio ratli 20 zilizopimwa kwa mizani ya Patakatifu, tena pishi moja ya mafuta ya chekele. Kisha uyatengeneze kuwa mafuta matakatifu ya kupaka kwa kuchanganya mafuta na manukato, kama mtengeneza manukato aliye fundi anavyojua kuyatengeneza, yapate kuwa kweli mafuta matakatifu ya kupaka. Kisha kwa hayo mafuta ulipake Hema la Mkutano na Sanduku la Ushahidi, na meza na vyombo vyake vyote na kinara na vyombo vyake na meza ya kuvukizia, na meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko na vyombo vyake vyote na birika na wekeo lake, uvitakase hivyo, vipate kuwa vitakatifu vyenyewe. Kisha kila atakayevigusa sharti awe ametolewa kuwa mtakatifu. Naye Haroni na wanawe uwapake mafuta, uwatakase, wapate kuwa watambikaji wangu. Nao wana wa Isiraeli uwaambie kwamba: Hayo mafuta ya kupaka sharti yawe matakatifu kwa vizazi vyenu, kwa kuwa ni yangu. Msiyamiminie mwilini mwa mtu, wala msitengeneze yaliyo sawa kama hayo, kwani ndiyo matakatifu, nayo sharti yawe matakatifu kwenu. Mtu atakayechanganya mafuta kuwa kama hayo au atakayeyapaka mtu mgeni sharti ang'olewe kwao walio ukoo wake. Bwana akamwambia Mose: Chukua viungo vinukavyo vizuri: liwa na udi na sandarusi, ndio viungo vinukavyo vizuri, tena uvumba ulio safi, vyote viwe kipimo kimoja tu. Uvitengeneze kuwa mavukizo, kama mtengeneza manukato aliye fundi anavyojua kuyatengeneza na kutia chumvi humo, yapate kutakata na kuwa matakatifu. Kisha uchukue humo kidogo, uyaponde sana, yawe kama uvumbi, kisha uchukue humo kidogo kuyaweka mbele ya Sanduku la Ushahidi katika Hema la Mkutano, nitakamokutana na wewe. Hayo mavukizo sharti yawe kwenu matakatifu yenyewe. Mavukizo mengine mtakayoyatengeneza, msiyatengeneze kuwa kama hayo, ila hayo sharti yawe matakatifu kwenu kwa kuwa yake Bwana. Mtu atakayetengeneza mavukizo kama hayo ya kuyavukiza sharti ang'olewe kwao walio wa ukoo wake. Bwana akamwambia Mose kwamba: Tazama, nimemwita kwa jina lake Besaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa shina la Yuda. Nikamjaza roho yangu ya Kimungu na kumgawia werevu wa kweli na utambuzi na ujuzi wa kutengeneza kazi yo yote, ajue kuvumbua kazi nzuri za ufundi wa kufua dhahabu na fedha na shaba; naye ni fundi wa kukatakata vito na kuvizungushia vikingo na fundi wa kuchora miti na fundi wa kufanya kazi yo yote. Tena tazama, mimi nimempa Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa shina la Dani, kuwa mwenzake. Namo mioyoni mwao wote walio werevu wa kweli nimetia werevu wa kweli, wayafanye yote, niliyokuagiza: Hema la Mkutano na Sanduku la Ushahidi na Kiti cha Upozi kilichoko juu yake na vyombo vyote vya hilo Hema, na meza na vyombo vyake, na kinara cha dhahabu tupu na vyombo vyake vyote na meza ya kuvukizia, na meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko na vyombo vyake vyote na birika na wekeo lake, na nguo nzuri za mapazia na mavazi matakatifu ya mtambikaji Haroni na mavazi ya wanawe, wapate kuwa watambikaji, na mafuta ya kupata na mavukizo yanukayo vizuri ya kuvukizia Patakatifu. Yote pia, niliyokuagiza, watayafanyiza vivyo hivyo. Bwana akamwambia Mose kwamba: Wewe sema na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Ziangalieni siku zangu za mapumziko, ziwe kielekezo cha Agano, nililoliagana nanyi, wao wa vizazi vyenu vijavyo wajue, ya kuwa mimi Bwana ndimi mwenye kuwatakasa ninyi. Kwa hiyo iangalieni siku ya mapumziko, ipate kuwa takatifu kwenu. Atakayelivunja hili agizo la kuitakasa hana budi kufa, kwani kila atakayefanya kazi siku hiyo, roho yake sharti ing'olewe kwao walio wa ukoo wake. Kazi na zifanywe siku sita, lakini siku ya saba ni siku ya sabato, ndio ya mapumziko kabisa, kwani ni siku takatifu ya Bwana. Kila atakayefanya kazi siku hiyo ya mapumziko hana budi kufa. Kwa hiyo wana wa Isiraeli sharti waiangalie siku ya mapumziko, huku kuiangalia siku ya mapumziko wakufanye kuwa agano la kale na kale kwa vizazi vyao. Hiki ni kielekezo cha kale na kale cha Agano, nililoliagana na wana wa Isiraeli, kwani Bwana alifanya kazi siku sita alipoziumba mbingu na nchi, lakini siku ya saba alipumzika na kutulia. Bwana alipokwisha kusema na Mose akampa kule mlimani kwa Sinai mbao mbili za Ushahidi, nazo zilikuwa za mawe zenye machoro, Mungu aliyoyachora kwa kidole chake. Watu walipoona, ya kuwa Mose anakawia kushuka mlimani, watu wakamkusanyikia Haroni, wakamwambia: Haya! Tufanyie miungu itakayotuongoza! Kwani hatuyajui yaliyompata huyo Mose aliyetutoa katika nchi ya Misri. Haroni akawaambia: Ziondoeni pete za dhahabu masikioni kwa wake zenu na kwa wana wenu wa kiume na wa kike, mniletee! Ndipo, watu wote walipoziondoa pete za dhahabu za masikioni kwao, wakampelekea Haroni. Akazichukua mikononi mwao, akazivunjavunja kwa patasi, akaziyeyusha, akazitengeneza kuwa ndama. Ndipo, waliposema: Huyu ndiye Mungu wako, Isiraeli, aliyekutoa katika nchi ya Misri. Haroni alipoyaona, akajenga mbele yake pa kutambikia, kisha Haroni akatangaza kwamba: Kesho ni sikukuu ya Bwana. Kesho yake wakaamka na mapema, wakatoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima pamoja na kuleta ng'ombe za tambiko za shukrani. Kisha watu wakakalia kula na kunywa, kisha wakainukia kucheza. Lakini Bwana akamwambia Mose: Nenda kushuka! Kwani wao walio ukoo wako, uliowatoa katika nchi ya Misri, wamefanya mabaya Wakiondoka upesi katika njia, niliyowaagiza; wamejitengenezea ndama kwa kuyeyusha dhahabu, wakaiangukia na kuitambikia wakisema: Huyu ndiye Mungu wako, Isiraeli, aliyekutoa katika nchi ya Misri. Bwana akamwambia Mose: Nikiwatazama watu hawa ninawaona kuwa watu wenye kosi ngumu. Sasa niache, makali yangu yawawakie moto, uwale! Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa. Lakini Mose akambembeleza Bwana Mungu wake kwamba: Bwana, mbona utayaacha makali yako, yawawakie watu wako, uliowatoa katika nchi ya Misri kwa uwezo mkuu na kwa mkono ulio na nguvu? Mbona unataka, Wamisri waseme kwamba: Aliwatoa kwa ubaya, awaue milimani na kuwatowesha juu ya nchi? Geuka na kuyaacha makali yako yanayowaka moto, uwahurumie walio ukoo wako kwa ajili ya mabaya, waliyoyafanya! Wakumbuke watumishi wako, Aburahamu na Isaka na Isiraeli, uliowaapia ukijitaja mwenyewe na kuwaambia: Wa uzao wenu nitawafanya kuwa wengi kama nyota za mbinguni, nayo nchi hiyo yote, niliyoisema, nitawapa wao wa uzao wenu, waichukue kuwa yao kale na kale. Ndipo, Bwana alipogeuza moyo, asiwafanyie hayo mabaya, aliyoyasema, ya kuwa atawafanyizia wao walio ukoo wake. Kisha Mose akageuka, akatelemka mlimani akizishika zile mbao mbili za Ushahidi mkononi mwake, nazo hizo mbao zilikuwa zimeandikwa pande zao zote mbili, kweli zilikuwa zimeandikwa huku na huko. Tena hizi mbao zilikuwa kazi ya Mungu, nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu mwenyewe yaliyochorwa humo mbaoni. Yosua alipozisikia sauti za makelele, watu waliyoyapiga, akamwambia Mose: Yako makelele makambini kama ya vita. Akajibu: Haya siyo makelele ya wapiga vita walioshinda, wala siyo makelele yao walioshindwa, mimi ninasikia tu sauti zao wanaoitikiana na kuimba. Mose alipoyafikia makambi karibu na kuona, jinsi hiyo ndama ilivyochezewa, ndipo, makali yake yalipowaka, akazitupa zile mbao, alizozishika mikononi mwake, akazivunja mlimani chini. Kisha akaichukua hiyo ndama, waliyoitengeza, akaitekeketeza kwa moto, akaipondaponda kuwa majivu, akayamwaga majini, akawapa wana wa Isiraeli, wayanywe. Kisha Mose akamwuliza Haroni: Watu hawa wamekukosea nini, ukiwakosesha kosa kubwa kama hili? Haroni akamwambia: Bwana wangu, makali yako yasiwake moto! Unawajua watu hawa, ya kuwa ni wabaya. Waliniambia: Tufanyie miungu itakayotuongoza! Kwani hatuyajui yaliyompata huyo Mose aliyetutoa katika nchi ya Misri. Nikawaambia: Kila mwenye dhahabu na aziondoe kwake, anipe mimi! Basi, waliponipa, nikazitupa motoni, ikatoka ndama hii. Mose alipoona, ya kuwa watu wanajikweza sana, kwa kuwa Haroni amewakweza, wafyozwe vibaya nao wawainukiao, ndipo, Mose alipokwenda kusimama langoni penye makambi, akasema: Aliye wa Bwana na aje kwangu! Ndipo, wana wa Lawi walipokusanyika wote kwake, akawaambia: Hivi ndivyo, alivyosema Bwana Mungu wa Isiraeli: Jifungeni kila mtu upanga wake kiunoni pake, mzunguke makambini kwenda na kurudi toka lango la huku hata lango la huko, mkiua kila mtu ndugu yake naye mwenzake naye rafiki yake! Wana wa Lawi wakayafanya, Mose aliyowaambia, wakauawa siku hiyo watu wa ukoo huo kama 3000. Kisha Mose akawaambia: Yajazeni leo magao yenu, mwe wa Bwana, maana kila mmoja wenu hakumjua wala mtoto wake wala ndugu yake; Bwana na awape leo mbaraka! Ikawa kesho yake, ndipo, Mose alipowaambia watu: Ninyi mmekosa kosa kubwa; sasa nitapanda kwenda kwa Bwana, nitazame, kama nitaweza kuwapatia upozi kwa ajili ya kosa lenu. Mose aliporudi kwa Bwana akamwambia: Watu wa ukoo huu wamekosa kosa kubwa wakijifanyizia mungu wa dhahabu. Lakini sasa uwaondolee kosa lao! Kama haiwezekani, lifute jina langu katika Kitabu chako, ulichokiandika! Naye Bwana akamwambia Mose: Anikoseaye ndiye, nitakayemfuta katika Kitabu changu. Sasa nenda, uwapeleke watu hawa hapo, nilipokuambia! Naye malaika wangu utamwona, akikutangulia. Lakini siku yangu ya mapatilizo itakapofika, nitawapatilizia hili kosa lao. Ndivyo, Bwana alivyowapiga watu wa huo ukoo kwa kuifanya hiyo ndama, Haroni aliyoifanya. Bwana akamwambia Mose: Nenda, uondoke hapa, wewe na watu hawa, niliowatoa katika nchi ya Misri, uwapeleke katika nchi ile, niliyomwapia Aburahamu na Isaka na Yakobo kwamba: Nchi hii nitawapa wao wa uzao wako. Nami nitamtuma malaika wangu, akutangulie; tena nitawafukuza Wakanaani na Waamori na Wahiti na Waperizi, Wahiwi na Wayebusi. Nchi ile ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali. Mwenyewe sitakuja kwenda katikati yenu, kwani m watu wenye kosi ngumu nisije kuwala njiani. Watu walipolisikia hili neno baya wakasikitika, wala hakuonekana mtu aliyeyavaa mapambo yake, kwa kuwa Bwana alimwambia Mose: Waambie wana wa Isiraeli: Ninyi m watu wenye kosi ngumu; kama ningekuwa katikati yenu kitambo kimoja tu, ningewamaliza. Kwa hiyo sasa jipambueni mapambo yenu, nijue, nitakavyowafanyizia! Kwa hiyo wana wa Isiraeli wakayavua mapambo yao huko mlimani kwa Horebu. Mose akaambiwa, lile Hema alichukue kila mara, alipige nje ya makambi, iwe mbali ya makambi, nalo aliite Hema la Mkutano, kila atakayemtafuta Bwana atoke kwenda kwenye Hema la Mkutano lililoko nje ya makambi. Napo, Mose atakapotoka kwenda kwenye Hema, watu wote na wainuke kusimama pa kuyaingilia mahema yao, watazame nyuma yake, hata aingie Hemani! Tena itakuwa, Mose atakapoingia Hemani, lile wingu lililo kama nguzo litashuka na kusimama hapo pa kuliingilia Hema, Bwana akisema na Mose. Watu wote watakapoliona hilo wingu lililo kama nguzo, likisimama hapo pa kuliingilia Hema, ndipo watu wote wainuke, wajiangushe chini kila mtu pa kuliingilia hema lake. Bwana atakapokwisha kusema na Mose uso kwa uso, kama mtu anavyosema na mwenzake, Mose na arudi makambini; lakini mtumishi wake Yosua, mwana wa Nuni, aliye kijana bado, asiondoke mle Hemani. Mose akamwambia Bwana: Tazama, wewe unaniambia: Wapeleke watu hawa! Lakini hujanijulisha bado, kama ni nani, utakayemtuma kwenda na mimi; tena ulisema: Ninakujua kwa jina, maana umeona upendeleo machoni pangu. Sasa kama nimeona kweli upendeleo machoni pako, unijulishe njia yako, nikujue, kwa kuwa niliona upendeleo machoni pako. Tena watazame watu hawa, kwani ndio taifa lako. Akamwambia: Uso wangu utakwenda na wewe, ukuongoze. Naye akamwambia: Uso wako usipokwenda na sisi, usitutoe huku kwenda huko! Ijulikane kwa nini, ya kuwa tumeona upendeleo machoni pako mimi nao walio ukoo wako, isipokuwa, wewe ukienda na sisi, tujulikane mimi nao walio ukoo wako, ya kuwa tumechaguliwa katika makabila yote yaliyoko juu ya nchi? Bwana akamwambia Mose: Neno hili, ulilolisema, nitalifanya nalo, kwani umeona upendeleo machoni pangu, nami ninakujua kwa jina. Mose akaomba: Nionyeshe utukufu wako! Akaitikia kwamba: Nitaupitisha wema wangu wote machoni pako, nalo Jina langu la Bwana nitalitamka kwa sauti kuu masikioni pako. Mimi nitakayemhurumia, nitamhurumia kweli; nitakayemwonea uchungu, nitamwonea uchungu wa kweli. Akamwambia tena: Lakini uso wangu huwezi kuuona, kwani hakuna mtu atakayekuwa yu hai akiisha kuniona. Bwana akamwambia tena: Nitakuonyesha mahali, ndipo upate kusimama juu ya mwamba. Hapo, utukufu wangu utakapopita, nitakuweka katika pango la huo mwamba na kukukingia kwa mkono wangu, mpaka nitakapokwisha kupita. Nitakapouondoa mkono wangu, utaweza kutazama nyuma yangu, lakini uso wangu mtu hawezi kuuona. Bwana akamwambia Mose: Jichongee mbao mbili za mawe, kama zile za kwanza zilivyokuwa! Nami nitaziandika hizo mbao maneno yale yaliyokuwa katika zile mbao za kwanza, ulizozivunja. Uwe tayari asubuhi, upate kupanda asubuhi mlimani kwa Sinai, usimame kwangu mlimani kwa Sinai. Asipande mtu pamoja na wewe, wala asionekane mtu mlimani po pote, wala kondoo wala mbuzi wala ng'ombe wasilishe penye mlima huu! Ndipo, alipochonga mbao mbili za mawe, kama zile za kwanza zilivyokuwa, Kisha Mose akajidamka asubuhi, akapanda mlimani kwa Sinai, kama Bwana alivyomwagiza, akizishika hizo mbao mbili mkononi mwake. Ndipo, Bwana aliposhuka winguni, akaja kusimama naye huko, akalitamka Jina la Bwana kwa sauti kuu, kisha Bwana akapita machoni pake na kutangaza: Bwana, Bwana ni Mungu mwenye huruma na utu, tena ni mwenye uvumilivu na upole na welekevu mwingi. Huwekea watu maelfu na maelfu magawio, huondoa manza na mapotovu na makosa, mbele yake hakuna asiye mkosaji; nazo manza, baba walizozikora, huzilipisha watoto na watoto wa watoto, akifikishe kizazi cha tatu na cha nne. Ndipo, Mose alipoinama chini upesi na kujiangusha usoni, akasema: Bwana wangu, kama nimeona upendeleo machoni pako, Bwana wangu na aende katikati yetu! Kwani watu hawa ni wenye kosi ngumu. Nawe tuondolee manza zetu na makosa yetu na kutupokea kuwa wako! Bwana akasema: Tazama, na nifanye agano mbele yao wote walio ukoo wako, nifanye vioja visivyofanyika katika nchi zote na kwa mataifa yote. Ndipo, watu wote, ambao uko katikati yao, watakapoyaona matendo ya Bwana, kwani hayo, nitakayoyafanya kwako, yatatisha. Yaangalie tu, ninayokuagiza leo! Utaniona, nikiwafukuza mbele yako Waamori na Wakanaani na Wahiti na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi. Jiangalie, usifanye agano na wenyeji wa nchi ile, utakayoiingia, wasiwe katikati yenu kama matanzi! Pao pa kutambikia sharti upabomoe, nazo nguzo zao za kutambikia sharti uzivunje, nayo miti yao ya Ashera sharti uikate! Usiangukie mungu mwingine! Kwani Bwana huitwa mwenye wivu, naye ni Mungu mwenye wivu kweli. Kwa hiyo usifanye agano na wenyeji wa nchi hiyo! Wao wakiifuata miungu yao pamoja na kufanya ugoni, tena wakiichinjia miungu yao ng'ombe za tambiko, wasikualike kula nyama za ng'ombe za tambiko. Wala usiwachukulie wanao wa kiume wake kwa wana wao wa kike, nao wangewafanyisha wanao ugoni wa kuifuata miungu yao, wao wakiifuata miungu yao kufanya ugoni. Usijifanyizie miungu kwa kuyeyusha yo yote. Sikukuu ya Mikate isiyochachwa uiangalie: siku saba ule mikate isiyochachwa, kama nilivyokuagiza; nazo siku zake zilizowekwa ni za mwezi wa Abibu, kwani katika mwezi wa Abibu ulitoka Misri. Kila aliye mwana wa kwanza wa mama yake awe wangu, hata kwa nyama wako wa kufuga kila mwana wa kiume wa kwanza ni wangu, kama ni ng'ombe au kondoo. Mwana wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana kondoo; usipomkomboa, umvunje shingo! Wana wa kwanza wote watakaozaliwa na wanao sharti uwakomboe. Watu wasinitokee mikono mitupu! Siku sita sharti ufanye kazi, lakini siku ya saba sharti upumzike, ijapo siku ziwe za kulima au za kuvuna, sharti upumzike. Nayo sikukuu ya Majuma saba (Pentekote) ishike kwako kuwa sikukuu ya Malimbuko ya ngano, nayo sikukuu ya kukusanya mapato ya mashambani mwisho wa mwaka uishike! Kila mwaka mara tatu waume wako wote sharti watokee mbele ya Bwana Mungu aliye Mungu wa Isiraeli. Kwani nitawafukuza wamizimu mbele yako, niipanue mipaka yako; hatakuwako mtu atakayeitamani nchi yako, utakapopanda kutokea mbele ya Bwana Mungu wako mara tatu kila mwaka. Usichinje, ng'ombe yangu ya tambiko, damu yake ikimiminikia panapo chachu yo yote, wala nyama za ng'ombe ya tambiko ya sikukuu ya Pasaka zisilale mpaka kesho. Malimbuko ya kwanza ya mashamba yako sharti uyapeleke Nyumbani mwa Bwana Mungu wako. Kitoto cha mbuzi usikipike katika maziwa ya mama yake. Bwana akamwambia Mose: Yaandike maneno haya yote! Kwani kwa maneno haya nimefanya agano na wewe nao wana wa Isiraeli. Akawa huko pamoja na Bwana siku 40 mchana na usiku, hakula chakula, wala hakunywa maji, akaandika katika zile mbao mbili maneno ya Agano hili, ndiyo yale maagizo kumi. Ikawa, Mose aliposhuka mlimani kwa Sinai alizishika hizo mbao mbili za Ushahidi mkononi mwake na kushuka mlimani kwa Sinai; hapo yeye Mose alikuwa hajui, ya kama ngozi ya uso wake inaangaza kwa kusema na Bwana. Haroni na wana wa Isiraeli walipomwona Mose, mara wakaona, ya kama ngozi ya uso wake inaangaza; ndipo, walipoogopa kumkaribia. Mose alipowaita, wakarudi kwake, Haroni nao watu wote walio wakuu penye mkutano wakarudi kwake, naye Mose akasema nao. Baadaye wana wote wa Isiraeli wakamkaribia, akawaagiza yote, Bwana aliyomwambia mlimani kwa Sinai. Mose alipokwisha kusema nao akaufunika uso wake kwa mharuma. Lakini Mose alipomtokea Bwana kusema naye akauondoa huo mharuma, mpaka atoke kwake. Naye alipotoka kwake, aseme na wana wa Isiraeli na kuwaambia aliyoagizwa, wana wa Isiraeli wakauona uso wake, ya kuwa uso wa Mose unaangaza; ndipo, Mose alipourudisha mharuma usoni pake, mpaka aingie tena kusema na Bwana. Mose akaukutanisha mkutano wote wa wana wa Isiraeli, akawaambia: Haya maneno ndiyo, Bwana aliyowaagiza kuyafanya. Kazi na zifanywe siku sita, lakini siku ya saba sharti iwe takatifu kwenu kuwa siku ya Bwana ya kupumzika kabisa. Kila atakayefanya siku hiyo kazi yo yote hana budi kuuawa. Msiwashe moto siku ya mapumziko po pote, mtakapokaa. Kisha Mose akauambia mkutano wote wa wana wa Isiraeli kwamba: Hili nalo ni neno, Bwana aliloliagiza kwamba: Mchangieni Bwana kwenu vipaji vya tambiko, kila mtu na avilete hivyo vipaji vya tambiko vya kumpa Bwana, kama moyo wake unavyomtuma: dhahabu na fedha na shaba, na nguo za kifalme na nywele za mbuzi, na ngozi nyekundu za madume ya kondoo na ngozi za pomboo na migunga, na mafuta ya taa na manukato ya kutengeneza mafuta ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri, na vito vya oniki na vito vingine vya kutia katika kisibau cha mtambikaji mkuu na katika kibati cha kifuani. Nao wote walio wenye werevu wa kweli mioyoni kwenu na waje kuyatengeneza yote, Bwana aliyoyaagiza: Kao lenyewe pamoja na Hema lake na chandalua chake na vifungo vyake na mbao zake na misunguo yake na nguzo zake na miguu yao; lile Sanduku (la ushahidi) na mipiko yake na Kiti cha Upozi na pazia la kukifungia; meza na mipiko yake na vyombo vyake vyote na mikate ya kuwa usoni pa Bwana; kinara cha kuangazia na vyombo vyake na taa zake na mafuta ya kuwasha; meza ya kuvukizia na mipiko yake na mafuta ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri na nguo za pazia ya hapo pa kuliingilia Kao; meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko pamoja na wavu wake wa shaba na mipiko yake na vyombo vyake vyote na birika na wekeo lake; nguo za ua na nguzo zake na miguu yake na pazia la langoni kwa ua; mambo za Kao na mambo za ua pamoja na kamba zao; na nguo nzuri za mapazia za kutumiwa Patakatifu na mavazi matakatifu ya mtambikaji Haroni na mavazi ya wanawe, wapate kuwa watambikaji. Ndipo, watu wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli walipotoka kwa Mose. Kisha watu wote wakaja kwa kuhimizwa na mioyo yao na kwa kutumwa na roho zao, wakaleta vipaji vyao vya tambiko vya kumpa Bwana vya kulitengeneza Hema la Mkutano na vya kutumiwa kwa kazi zake zote na vya nguo za Patakatifu. Wakaja waume kwa wake, maana wote walitumwa na mioyo yao, wakaleta vipini na mapete ya masikioni na pete za vidoleni na mapambo yo yote ya dhahabu; tena kila mtu akaleta dhahabu kuwa vipaji vya tambiko vya kupitishwa motoni vya kumpa Bwana. Kila mtu aliyeona kwake nguo ya kifalme nyeusi au nyekundu au nguo ya bafta au nywele za mbuzi au ngozi nyekundu za madume ya kondoo au ngozi za pomboo, akazileta. Nao wote waliotaka kutoa fedha na shaba kuwa vipaji vyao vya tambiko wakazileta kumpa Bwana hivyo vipaji vya tambiko. Nao wote walioona kwao miti ya migunga iliyofaa kutumiwa kwa kazi yo yote wakaileta. Nao wanawake waliokuwa wenye ujuzi huo mioyoni mwao wakasokota nyuzi kwa mikono yao, kisha wakazileta hizo nyuzi, walizozisokota za kufuma nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na nguo za bafta. Nao wanawake wote waliohimizwa na mioyo yao kwa kuijua vema kazi hiyo wakasokota nywele za mbuzi. Nao wakuu wakaleta vito vya oniki na vito vingine vya kutiwa katika kisibau cha mtambikaji mkuu na katika kibati cha kifuani, na manukato na mafuta ya taa na ya kutengeneza mafuta ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri. Hivyo wakachanga wana wa Isiraeli wote, waume kwa wake, waliotumwa na mioyo yao kuyapeleka yafaayo ya kufanya kazi zote, Bwana alizoziagiza kinywani mwa Mose, zifanywe. Kisha Mose akawaambia wana wa Israeli: Tazameni, Bwana amemwita kwa jina lake Besaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa shina la Yuda; akamjaza roho yake ya Kimungu na kumgawia werevu wa kweli na utambuzi na ujuzi wa kutengeneza kazi yo yote, ajue kuvumbua kazi nzuri za ufundi wa kufua dhahabu na fedha na shaba; naye ni fundi wa kukatakata vito na kuvizungushia vikingo na fundi wa kuchora miti na fundi wa kufanya kazi zote za ufundi. Tena akampa moyoni mwake uwezo wa kufundisha wengine, yeye na mwenzake Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa shina la Dani. Mioyo yao aliijaza werevu wa kweli, wafanye kazi zo zote: kuchora kwa ufundi ulio werevu wa kweli, kufuma nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na nguo za bafta, kama mafundi wa kufuma nguo wanavyojua, kufanya kazi zote pia, hata kuvumbua kazi nzuri zisizofanyika bado. Besaleli na Oholiabu na watu wote, Bwana aliowapa werevu wa kweli mioyoni mwao, watazifanya kazi hizo kwa huo werevu wa kweli na kwa utambuzi na kwa hivyo, wanavyojua kufanya kazi zote za utumishi wa Patakatifu, watafanya yote, Bwana aliyoyaagiza. Kisha Mose akawaita Besaleli na Oholiabu na watu wote waliokuwa werevu wa kweli mioyoni mwao, Bwana aliowapa werevu wa kweli mioyoni mwao, nao wote waliohimizwa na mioyo yao kuzijia hizo kazi, wazifanye. Wakachukua kwake Mose vipaji vyote vya tambiko, wana wa Isiraeli walivyovitoa vya kazi za utumishi wa Patakatifu, zipate kufanyika; nao walikuwa wakileta bado kwake vipaji, walivyovitoa kwa kupendezwa tu kila kulipokucha. Kisha wakaja wote waliokuwa werevu wa kweli wa kuzifanya hizo kazi zote za Patakatifu, kila mmoja wakitoka penye kazi zao, walizozifanya wao, wakamwambia Mose kwamba: Watu wanaleta mengi zaidi kabisa kuliko yanayotakiwa ya kuzimaliza hizo kazi, Bwana alizoagiza kuzifanya. Ndipo, Mose alipotoa amri, wakaitangaza makambini po pote kwa sauti kuu kwamba: Watu wote, waume kwa wake, wasijisumbue tena kutoa vipaji vya tambiko vya hapo Patakatifu! Ndivyo, watu walivyozuiliwa kuleta vitu tena. Nayo yaliyokuwapo hapo ya kuzifanya hizo kazi yakatosha kabisa kuzifanya hizo kazi zote pia, tena yakasalia. Miongoni mwao waliofanya kazi wao wote waliokuwa werevu wa kweli mioyoni mwao wakalitengeneza Kao lenyewe kwa mapazia kumi yaliyoshonwa kwa nguo za bafta ngumu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu, nayo yalikuwa yenye mifano ya Makerubi, kama mafundi wa kufuma wanavyojua kuitengeneza; ndivyo, walivyofanya. Urefu wa pazia moja ulikuwa mikono ishirini na minane, nao upana wake ulikuwa mikono minne, kila pazia moja lilikuwa lenye kipimo hiki kimoja, kilikuwa cha mapazia yote. Akaunga mapazia matano kila moja na mwenzake kuwa moja, nayo matano ya pili akayaunga vivyo hivyo kila moja na mwenzake kuwa moja. Kisha akashona vitanzi vya nguo nyeusi za kifalme penye upindo wa nje wa kila pazia moja hapo, lilipoungwa na jingine; vivyo hivyo akavitia napo penye yupindo wa nje wa kila pazia la pili hapo, lilipoungwa nalo la kwanza. Akashona vitanzi hamsini katika kila pazia moja upande mmoja, na tena vitanzi hamsini katika upindo wa kila pazia la pili upande huo ulioungwa na pazia la kwanza; hivyo vitanzi vilielekeana kila kimoja na mwenzake. Kisha akafanya vifungo vya dhahabu hamsini, apate kuyafunga mapazia kila moja na mwenzake; kwa hivyo vifungo Kao likapata kuwa moja. Kisha akafanya mapazia ya nywele za mbuzi kuwa hema juu ya Kao lenyewe, akatengeneza mapazia kumi na moja. Urefu a kila pazia moja ulikuwa mikono thelathini, nao upana wa kila pazia moja ulikuwa mikono minne; hiki kipimo kimoja kilikuwa chao mapazia yote kumi na moja. Kisha akayaunga mapazia matano kuwa moja, nayo yale sita akayaunga kuwa moja. Kisha akashona vitanzi hamsini katika upindo wa nje wa kila pazia moja hapo, lilipoungwa na jingine; tena akashona vitanzi hamsini katika upindo wa nje wa kila pazia la pili hapo, lilipoungwa nalo la kwanza. Kisha akafanya vifungo vya shaba hamsini vya kuliungia hilo hema, liwe moja. Kisha akatengeneza chandalua cha hema kwa ngozi nyekundu za madume ya kondoo, tena akatengneza chandalua cha pili kwa ngozi za pomboo kuwa juu yake. Kisha akatengeneza mbao za Kao lenyewe za migunga zilizosimama. Urefu wa kila ubao ulikuwa mikono kumi, nao upana wake kila ubao mmoja ulikuwa mkono mmoja na nusu. Kila ubao mmoja ulikuwa na vigerezi viwili, navyo vilitazamana kila kimoja na mwenzake. Vivyo hivyo akavitengeneza kila ubao mmoja wa Kao lenyewe. Akazitengeneza hizo mbao za Kao lenyewe kuwa ishirini upande wa kusini, ndio upande wa juani. Chini ya hizi mbao ishirini akatengeneza viguu vya fedha arobaini, vikawa viguu viwili chini ya kila ubao mmoja vya kuvitilia vigerezi vyake viwili, vivyo hivyo chini ya kila ubao mmoja viguu viwili vya kuvitilia vigerezi vyake viwili. Hata upande wa pili wa Kao, ndio upande wa kaskazini, akatengeneza vilevile mbao ishirini, na viguu arobaini vya fedha, viguu viwili chini ya kila ubao mmoja, vivyo hivyo viwili chini ya kila ubao mmoja. Lakini upande wa nyuma wa Kao unaoelekea baharini akatengeneza mbao sita. Tena akatengeneza mbao mbili za pembeni mle Kaoni upande wa nyuma. Nazo zilikuwa kama pacha, toka chini viliendelea pamoja zote nzima mpaka juu penye pete la kwanza; hivyo ndivyo, alivyozitengeneza mbao zote mbili za hizo pembe mbili za nyuma. Hivyo zote pamoja zilikuwa mbao nane, navyo viguu vya fedha vilikuwa kumi na sita, viguu viwili chini ya kila ubao mmoja. Kisha akatengeneza misunguo ya migunga, mitano ya mbao za upande mmoja wa Kao, tena misunguo mitano ya mbao za upande wa pili wa Kao, tena misunguo mitano ya mbao za upande wa nyuma wa Kao unaoelekea baharini. Kisha akatengeneza msunguo wa katikati, upite katikati ya mbao toka mwisho wa huku hata mwisho wa huko. Nazo mbao akazifunikiza dhahabu, nayo mapete yao akayatengeneza kwa dhahabu, yalikuwa ya kutilia misunguo, nayo misunguo akaifunikiza dhahabu. Kisha akatengeneza pazia lililoshonwa kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu; lilikuwa kazi ya fundi wa kufuma, maana alilitengeneza kuwa lenye Makerubi. Kisha akalitengenezea nguzo nne za migunga, akazifunikiza dhahabu, navyo vifungo vyao vilikuwa vya dhahabu, kisha akazitengenezea miguu minne kwa kuyeyusha fedha. Napo hapo pa kuliingilia Hema akaweka guo kubwa lililotengenezwa kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu; nalo lilifumwa na mtu aliyejua kweli kufuma kwa nyuzi za rangi. Akalitengenezea nguzo tano zenye vifungo vyao. Kisha akazifunikiza dhahabu pamoja na vichwa vyao na vijiti vyao vya kuziungia, lakini miguu yao mitano ilikuwa ya shaba. Kisha Besaleli akalitengeneza Sanduku la mbao za migunga, urefu wake ulikuwa mikono miwili na nusu, nao upana wake ulikuwa mkono mmoja na nusu, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mkono mmoja na nusu. Akalifunikiza lote dhahabu tupu, upande wa ndani na upande wa nje, kisha akazungusha juu yake taji ya dhahabu. Kisha akatengeneza mapete manne kwa kuyeyusha dhahabu, akayatia penye pembe zake nne, mapete mawili upande wake mmoja, tena mapete mawili upande wake wa pili. Kisha akatengeneza mipiko ya migunga, nayo akaifunikiza dhahabu. Kisha akaitia mipiko hiyo katika yale mapete pande zote mbili za Sanduku, iwe ya kulichukulia Sanduku. Kisha akakitengeneza kifuniko kuwa Kiti cha Upozi cha dhahabu tupu, urefu wake ulikuwa mikono miwili na nusu, nao upana wake ulikuwa mkono mmoja na nusu. Kisha akatengeneza Makerubi mawili ya dhahabu, nayo yalitengenezwa kwa kuzifuafua hizo dhahabu, akayaweka pande zote mbili za mwisho wa Kiti cha Upozi: Kerubi moja akaliweka upande wa mwisho wa huku, nalo la pili upande wa mwisho wa huko. Ndivyo, alivyoyaweka hayo Makerubi pande zake zote mbili za mwisho wa Kiti cha Upozi. Nayo Makerubi yalikuwa yameyakunjua mabawa juu yakikifunika Kiti cha Upozi kwa mabawa yao, nazo nyuso zao zilikuwa zimeelekeana, hayo Makerubi yakikitazama Kiti cha Upozi kwa nyuso zao. Kisha akatengeneza meza kwa mbao za migunga, urefu wake ulikuwa mikono miwili, nao upana wake ulikuwa mkono mmoja, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mkono mmoja na nusu; akaifunikiza dhahabu tupu, kisha akazungusha juu yake taji ya dhahabu. Kisha akazungusha kando yake kibao cha kukingia chenye upana wa shibiri, nacho hicho kikingio akakizungushia taji ya dhahabu. Kisha akaitengenezea mapete manne kwa kuyeyusha dhahabu, nayo hayo mapete akayatia penye pembe zake nne zilizokuwa penye miguu yake minne. Hayo mapete yalikuwa papo hapo chini ya kikingio, wapate kutia humo mipiko ya kuichukulia hiyo meza. Kisha akatengeneza mipiko kwa migunga na kuifunikiza dhahabu, itumike ya kuichukulia hiyo meza. Kisha akatengeneza vyombo vya kuweka hapo mezani: vyano vyake na vijiko vyake na vikombe vyake na vitungi vyake vinavyotumikia vinywaji vya tambiko; vyote vilikuwa dhahabu tu. Kisha akatengeneza kinara cha dhahabu tupu; hicho kinara nacho akakitengeneza kwa kufuafua dhahabu, ikapata kukitoka chote kizima: shina lake na mti wake navyo vikombe vyake na vifundo vyake na maua yake, vyote pia vilikuwa vimetoka dhahabu iyo hiyo moja. Matawi sita yalitoka penye mbavu zake, matawi matatu ya kinara yalitoka penye ubavu mmoja, tena matawi matatu ya kinara yalitoka penye ubavu wa pili. Vikombe vitatu vilivyofanana na maua yao. Vivyo hivyo vilikuwa katika matawi yote sita yaliyotoka katika mti wa kinara. Lakini katika mti wa kinara vilikuwa vikombe vinne vilivyofanana na maua ya mlozi, yaani vifundo pamoja na maua yao. Tena kila mahali matawi mawili yalipotoka katika huo mti wake, chini yake kilikuwa kifundo kimoja; vilikuwa vivyo hivyo kila mahali, yalipotoka matawi mawili, nayo matawi yaliyotoka katika kinara yalikuwa sita. Vifundo na matawi yao yote ilikuwa kazi moja iliyoyatokeza yote pamoja kwa kuifua dhahabu iyo hiyo moja, nayo yalikuwa dhahabu tupu. Kisha akatengeneza taa zake saba; nazo koleo zake na makato yake yote yalikuwa dhahabu tupu. Alikitengeneza kinara pamoja na vyombo vyake kwa kipande cha dhahabu chenye uzito wa mizigo miwili. Kisha akatengeneza kwa migunga meza ya kuvukizia; urefu wake ulikuwa mkono mmoja, nao upana wake ulikuwa mkono mmoja, pande zote nne zilikuwa sawa, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono miwili. Akaifunikiza dhahabu tupu juu yake na kando yake pande zote na pembe zake, akazungusha juu yake taji ya dhahabu pande zote. Kisha akaitengenezea mapete mawili ya dhahabu, akayatia chini ya taji pande zake mbili penye mbavu zake mbili, yawe ya kutilia mipiko ya kuichukulia. Kisha akatengeneza mipiko kwa migunga, akaifunikiza dhahabu. Kisha akatengeneza mafuta matakatifu ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri yasiyochanganyika na mengine, kama mafundi wa kutengeneza manukato wanavyojua kuyatengeneza. Kisha akatengeneza kwa mbao za migunga meza ya kuteketezea ng'ome za tambiko; urefu wake ulikuwa mikono mitano, nao upana wake ulikuwa mikono mitano, pande zote nne zilikuwa sawa; nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono mitatu. Penye pembe zake nne akatengeneza pembe zilizoipasa, nazo hizo pembe zake zilikuwa za mti uo huo mmoja; kisha akaifunikiza shaba. Akatengeneza navyo vyombo vyote vya meza ya kutambikia: nyungu na majembe na vyano na nyuma na sinia; vyombo vyake vyote akavitengeneza kwa shaba. Kisha akaitengenezea meza ya kutambikia kikingio kilichofanana na wavu wa shaba, akauweka chini ya ukingo wake kuelekea chini, ufike mpaka katikati ya meza ya kutambikia. Kisha akatengeneza mapete manne kwa kuyeyusha shaba, akayatia katika hizo pembe nne za wavu wa shaba ya kutilia mipiko. Kisha akatengeneza mipiko ya migunga, akaifunikiza shaba. Hiyo mipiko akaitia katika hayo mapete yaliyokuwa pande mbili penye meza ya kutambikia, itumike ya kuichukulia. Hivyo meza ya kutambikia aliitengeneza kwa mbao, iwe yenye mvungu ndani ulio wazi. Kisha akatengeneza birika la shaba pamoja na wekeo lake la shaba, akitumia vioo vya shaba vya wanawake waliotumika hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Kisha akatengeneza ua upande wa kusini ulio wa juani; nguo za ua huo akazitengeneza kwa bafta ngumu, urefu wao ulikuwa mikono mia. Nguzo zao ishirini zilikuwa zenye miguu ishirini ya shaba, lakini vifungo vya nguzo na vijiti vyao vya kuziungia juu vilikuwa vya fedha. Hata upande wa kaskazini ulikuwa vivyo hivyo: nguo zilikuwa zenye urefu wa mikono mia, nazo nguzo zao ishirini zilikuwa zenye miguu ishirini ya shaba, lakini vifungo vya nguzo na vijiti vyao vya kuziungia juu vilikuwa vya fedha. Nao upande wa ua unaoelekea baharini ulikuwa wenye nguo za mikono hamsini, nazo nguzo zake zilikuwa kumi zenye miguu kumi, navyo vifungo vya nguzo na vijiti vyao vya kuziungia juu vilikuwa vya fedha. Nao upande wa maawioni kwa jua ulikuwa mikono hamsini. Nguo ya upande wa huku ilikuwa ya mikono kumi na mitano, nazo nguzo zake zilikuwa tatu zenye miguu mitatu. Nao upande wa huko nguo yake ilikuwa ya mikono kumi na mitano, maana hapo pa kuuingilia ua ulikuwa upande wa huku na upande wa huko, nazo nguzo zake zilikuwa tatu zenye miguu mitatu. Nguo zote za kuuzunguka ua zilikuwa za bafta ngumu. Miguu ya nguzo ilikuwa ya shaba, lakini vifungo vya nguzo na vijiti vyao vya kuziungia juu vilikuwa vya fedha, navyo vichwa vyao walivifunikiza fedha, nazo nguzo zote za ua zilikuwa zimeungwa kwa vijiti vya fedha. Hapo penye lango la ua palikuwa na pazia lililokuwa kazi ya fundi wa kufuma kwa nyuzi za rangi, nalo lilitengenezwa kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu, urefu ulikuwa mikono ishirini, nao upana wa kwenda juu ulikuwa mikono mitano, sawasawa kama nguo nyingine za ua. Nguzo zake nne pamoja na miguu yake minne zilikuwa za shaba, lakini vifungo vyao vilikuwa vya fedha, navyo vichwa vyao viliuwa vimefunikizwa fedha, navyo vijiti vyao vya kuziungia juu vilikuwa vya fedha. Lakini mambo zote za Kao lenyewe na za ua kuuzunguka wote zilikuwa za shaba. Hii ndio hesabu ya mali za kulitengeneza hilo Kao lililokuwa Kao la Ushahidi, nazo zilihesabiwa kwa agizo la Mose; walioifanya kazi hii ndio Walawi, nao waliangaliwa na Itamari, mwana wa mtambikaji Haroni. Besaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa shina la Yuda, alifanya yote, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Pamoja naye alifanya kazi Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa shila la Dani; naye alikuwa fundi wa kuchora na wa kuvumbua kazi nzuri za ufundi na wa kufuma kwa nyuzi za rangi za nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na za bafta ngumu. Dhahabu zote zilizotumika za kufanya kazi zote za kupatengeneza Patakatifu, zilikuwa dhahabu zilizotolewa kuwa vipaji vya tambiko vya kupitishwa motoni, nazo zilikuwa jumla talanta 29 na sekeli 730, pamoja ndio frasila 80 zikipimwa kwa mizani ya patakatifu. Nazo fedha zilizotolewa na mkutano kwa kukaguliwa zilikuwa jumla talanta 100 na sekeli 1775, pamoja ndio frasila 244 zikipimwa kwa izani ya Patakatifu. Kila kichwa walilipa beka moja, ndio nusu ya fedha au shilingi mbili kwa kipimo cha fedha cha Patakatifu; ndivyo, kila mmoja alivyolipa alipofika kukaguliwa kuwa ni mwenye miaka ishirini na zaidi, nao walikuwa watu 603550. Zile talanta 100 za fedha zilitumika za kuitengeneza miguu ya Patakatifu na miguu ya pazia kwa kuziyeyusha, miguu 100 kwa talanta 100, talanta moja ya mguu mmoja. Nazo zile sekeli 1775 zilitumika za kuvitengeneza vifungo vya nguzo na za kuvifunikiza vichwa vyao na za vijiti vya kuziungia juu. Nazo shaba vipaji vyake vya tambiko vya kupitishwa motoni vilikuwa talanta 70 na sekeli 2400, pamoja ndio frasila 230. Hizi zilitumika za kutengeneza miguu ya hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano na meza ya shaba ya kutambikia na wavu wa shaba uliotiwa kwake na vyombo vyote vya meza ya kutambikia, nayo miguu ya pande zote za uani na miguu ya langoni penye ua na mambo zote za Kao lenyewe na mambo za pande zote za uani. Zile nguo za kifalme nyeusi na nyekundu walizitumia za kutengeneza mavazi mazuri ya kutumikia Patakatifu, wakayatengeneza hayo mavazi matakatifu ya Haroni, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha walikitengeneza kisibau kwa dhahabu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu. Hizo dhahabu wakazisanasana kuwa mabati membamba, kisha wakayapasuapasua kuwa nyuzi, ziwezekane kufumwa pamoja na nyuzi za nguo za kifalme nyeusi na nyekundu, tena na nyuzi za bafta, kazi hii ilikuwa kazi ya ufundi wa kweli. Hicho kisibau kilikuwa chenye vipande viwili vilivyounganika mabegani, penye ncha zake mbili ndipo, kilipofungika. Nayo masombo yake ya kukifunga kifuani pake yalikuwa ya kazi iyo hiyo: yalitengenezwa kwa dhahabu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha wakatengeneza vito viwili vya oniki, wakavizungushia vikingo vya dhahabu vya kuvishika, nayo majina ya wana wa Isiraeli yakachorwa humo, kama machoro ya muhuri yanavyochorwa. Kisha akavibandika hivyo vito penye vile vipande viwili vya mabegani vya kisibau kuwa vito vya kumbukumbushia wana wa Isiraeli, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha wakakitengeneza kibati cha kifuani, nacho kilikuwa kazi ya ufundi wa kweli kama ile kazi ya kisibau, nacho kilitengenezwa kwa dhahabu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu. Pande zake zote zilikuwa sawasawa, tena hicho kibati kilikuwa kimekunjwa kuwa kuwili; urefu wake ulikuwa shibiri, nao upana wake ulikuwa shibiri, tena kilikuwa kimekunjwa kuwa kuwili. Wakakijaza vito na kuviweka kuwa mistari minne ya vito. Mstari wa kwanza: sardio, topazio na sumarato; ndio mstari wa kwanza. Mstari wa pili: almasi nyekundu, safiro na yaspi; mstari wa tatu: hiakinto, akate na ametisto; mstari wa nne: krisolito, oniki na berilo. Navyo vilipotiwa vyote vilikuwa vimezungushiwa vikingo vya dhahabu vya kuvishika. Hivyo vito vilikuwa kumi na viwili kwa hesabu ya majina ya wanawe Isiraeli vikiyafuata hayo majina yao, kila kimoja chao kilipata jina lake moja katika hayo mashina kumi na mawili, lilikuwa limechorwa humo, kama kazi ya muhuri ilivyo. Tena wakatengeneza kwa dhahabu tupu vikufu vilivyofanana na kamba zilizosokotwa, wakavitia penye kibati cha kifuani. Kisha wakatengeneza vipini viwili vya dhahabu na pete mbili za dhahabu, wakazitia hizo pete mbili penye zile ncha mbili za juu za kibati cha kifuani. Kisha hivyo vikufu viwili vya dhahabu vilivyofanana na kamba wakavifunga katika zile pete mbili penye zile ncha za juu za kibati cha kifuani. Kisha hiyo miisho mingine miwili ya hivyo vikufu viwili vilivyofanana na kamba wakaifunga katika vile vikingo viwili vya dhahabu, kisha wakavifunga penye vipande vya mabegani vya kisibau upande wake wa mbele. Kisha wakatengeneza tena pete mbili za dhahabu, wakazitia penye zile ncha mbili za chini za kibati cha kifuani katika upindo wake ulioko upande wa ndani uliokielekea kisibau. Kisha wakatengeneza tena pete mbili, wakazitia katika vipande vile viwili vya mabegani vya kisibau chini yake upande wake wa mbele papo hapo, vile vipande vilipounganika, juu ya masombo ya kisibau. Kisha wakakifunga kibati cha kifuani kwa kamba ya nguo nyeusi ya kifalme wakitia katika pete zake, tena katika pete za kisibau, kibati cha kifuani kipate kukaa juu ya masombo ya kisibau, kisiweze kusogeasogea hapo pake penye kisibau, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha wakatengeneza kanzu iliyokipasa hicho kisibau, nayo ilikuwa kazi ya fundi aliyejua kweli kufuma kwa nyuzi za rangi, yote nzima ilikuwa ya nguo nyeusi ya kifalme. Upande wa juu wa kanzu katikati yake ulikuwa na tundu lililofanana na tundu la shati ya chuma ya mpiga vita, kando lilizungukwa na taraza, lisipasuke. Penye upindo wa chini wa kanzu wakatengeneza komamanga kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu zilizo ngumu. Kisha wakatengeneza vikengele vidogo vya dhahabu tupu, wakavitia hivyo vikengele katikati ya komamanga kuuzunguka upindo wa chini wa kanzu po pote katikati ya komamanga, vikawa hivyo: kikengele kidogo na komamamnga, kikengele kidogo na komamanga, vivyo hivyo po pote kuuzunguka upindo wote wa chini wa kanzu, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Wakamtengenezea Haroni na wanawe shati za bafta, nayo ilikuwa kazi ya fundi aliyejua kufuma kweli. Wakatengeneza nacho kilemba na kofia ndefu za nguo za bafta na suruali nyeupe za ukonge na za nguo za bafta na za nguo za kifalme nyeusi na nyekundu, nayo ilikuwa kazi ya fundi aliyejua kufuma kwa nyuzi za rangi, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha wakatengeneza kwa dhahabu tupu bamba kuwa taji takatifu ya pajini, wakachora humo machoro yaliyokuwa kama machoro ya muhuri kwamba: Mtakatifu wa Bwana. Wakalifunga kwa kamba ya nguo nyeusi ya kifalme, wapate kulifunga vema katika kilemba upande wake wa mbele, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Hivyo ndivyo, kazi zote za kulitengeneza Kao la Hema la Mkutano zilivyokwisha, nao wana wa Isiraeli waliyafanya yote; kama Bwana alivyomwagiza Mose, waliyafanya yote kuwa sawasawa. Wakampelekea Mose hilo Kao: Hema na vyombo vyake vyote, vifungo, mbao, misunguo na nguzo zake pamoja na miguu, na chandalua cha ngozi nyekundu za madume ya kondoo na chandalua cha ngozi za pomboo na pazia kubwa la Hemani, Sanduku la Ushahidi pamoja na mipiko yake na Kiti cha Upozi, meza na vyombo vyake vyote na mikate ya kuwa usoni pa Bwana, kinara cha dhahabu tupu pamoja na taa zake zilizokuwa zimekwisha kupangwa mstari mmoja, na vyombo vyake vyote na mafuta ya taa, na meza ya dhahabu ya kuvukizia pamoja na mafuta ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri na pazia la hapo pa kuliingilia Hema, na meza ya shaba ya kutambikia pamoja na wavu wake wa shaba na mipiko yake na vyombo vyake vyote na birika pamoja na wekeo lake, na nguo za mapazia ya uani pamoja na nguzo zake na miguu yake, tena guo kubwa la pazia la langoni kwa ua pamoja na kamba zake na mambo zake na vyombo vyake vyote vya kutumikia katika hili Kao la Hema la Mkutano, tena mavazi mazuri ya kutumikia Patakatifu, ndiyo mavazi ya mtambikaji Haroni na mavazi ya wanawe ya kufanyia kazi za utambikaji. Wana wa Isiraeli waliyatengeneza yote na kuzifanya kazi hizi zote, ziwe sawasawa, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Mose alipoyatazama hayo yote, waliyoyafanya, akaona, ya kama wameyafanya kweli kuwa sawasawa, kama Bwana alivyoagiza; kwa hiyo Mose akawabariki. Bwana akamwambia Mose kwamba: Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza ulisimamishe Kao la Hema la Mkutano. Humo ndani uliweke Sanduku la Ushahidi, kisha ulitungike pazia mbele ya Sanduku. Kisha iingize meza na kuyatandika juu yake yanayopasa kuwekwa hapo, kisha kiingize kinara na kuziweka taa zake juu yake. Kisha iweke meza ya dhahabu ya kuvukizia mbele ya Sanduku la Ushahidi na kulitungika pazia pa kuliingilia Kao. Kisha iweke meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko mbele ya hapo pa kuliingilia Kao la Hema la Mkutano. Kisha uliweke birika katikati ya hema la Mkutano na meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko na kulitia maji. Kisha Kao ulizungushie ua na kulitungika guo la pazia la langoni kwa ua. Kisha yachukue mafuta ya kupaka, ulipake Kao lenyewe nayo yote yaliyomo; ndivyo, ulieue pamoja na vyombo vyake vyote kuwa vitakatifu. Kisha ipake mafuta meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, uieue, hiyo meza ya kutambikia ipate kuwa takatifu yenyewe. Kisha birika lipake mafuta nalo wekeo lake, ulieue. Kisha mwite Haroni nao wanawe, wafike hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, kisha waambie wajiogeshe majini. Kisha umvike Haroni mavazi matakatifu na kumpaka mafuta; hivi ndivyo, utakavyomweua, apate kuwa mtambikaji wangu. Kisha wafikishe wanawe karibu, uwavike shati, kisha wapake nao mafuta, kama ulivyompaka baba yao mafuta, wapate kuwa watambikaji wangu. Huko kuwapaka mafuta kutawapatia utambikaji wa kale na kale kwa vizazi vyao. Mose akayafanya yote; kama Bwana alivyomwagiza, ndivyo, alivyoyafanya yote sawasawa. Ikawa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, ndipo, Kao liliposimamishwa. Mose alipolisimamisha Kao akaiweka miguu yake, akatia humo mbao zake, akazitia misunguo yake na kuzisimamisha nguzo zake. Kisha akaweka juu ya Hema chandalua chake, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha akauchukua ushahidi, akauweka Sandukuni, akatia nayo mipiko penye Sanduku, akakiweka Kiti cha Upozi juu ya Sanduku. Kisha akaliingiza Sanduku Kaoni ndani, akalitungika lile guo kubwa la pazia, lilifiche Sanduku la Ushahidi, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha akapeleka meza ndani ya Hema la Mkutano, akaiweka upande wa kaskazini wa Kao nje ya pazia, kisha akamwekea Bwana juu yake mikate na kuitandika mistari mistari, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha akakiweka kinara Hemani mwa Mkutano upande wa kusini wa Kao, kuielekea meza. Kisha akaziweka taa zake juu yake mbele ya Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha akaiweka meza ya dhahabu ya kuvukizia katika Hema la Mkutano mbele ya pazia. Akavukizia juu yake mavukizo yanukayo vizuri, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha akalitungika pazia hapo pa kuliingilia Kao. Kisha akaiweka meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko penye kuliingilia Kao la Hema la Mkutano, akatoa juu yake ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima pamoja na vilaji vya tambiko, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha akaliweka birika katikati ya Hema la Mkutano na meza ya kutambikia na kutia humo maji ya kujioshea. Kisha Mose na Haroni na wanawe wakajiosha humo mikono yao na miguu yao. Kila walipoliingia Hema la Mkutano, napo kila walipoikaribia meza ya kutambikia wakajiosha, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha akausimamisha ua wa kulizunguka Kao na meza ya kutambikia, kisha akalitungika pazia langoni kwa ua. Ndivyo, Mose alivyozimaliza hizi kazi. Kisha lile wingu likalifunika Hema la Mkutano, nao utukufu wa Bwana ukajaa Kaoni. Naye Mose hakuweza kuliingia Hema la Mkutano, kwa kuwa wingu lililikalia, nao utukufu wa Bwana ulijaa Hemani. Hilo wingu lilipoondoka penye Kao, ndipo, wana wa Isiraeli walipoondoka kwenda safari yao; ndivyo, vilivyokuwa katika hizo safari zao zote. Lakini wingu lisipoondoka, hawakuondoka nao kwenda safari mpaka siku hiyo, lilipoondoka tena. Kwani wingu la Bwana lililikalia Kao mchana, lakini usiku ulikuwamo moto, nao wote walio wa mlango wa Isiraeli wakauona katika safari zao zote. Bwana akamwita Mose, akasema naye toka Hemani mwa Mkutano kwamba: Waambie wana wa Isiraeli na kuwaagiza hivyo: Mtu wa kwenu akitaka kumpelekea Bwana matoleo ya nyama wa kufuga sharti hayo matoleo yenu myatoe katika ng'ombe au katika mbuzi na kondoo. Kama toleo lake ni ng'ombe, anayemtoa kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, sharti atoe dume asiye na kilema, ampeleke pa kuliingilia Hema la Mkutano, Bwana apate kupendezwa naye. Kisha aubandike mkono wake kichwani pake hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, impatie upendezo wa kupozwa kwake. Kisha amchinje huyo mwana wa ng'ombe mbele ya Bwana, nao wana wa Haroni walio watambikaji na waipeleke damu, nayo hiyo damu wainyunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia iliyopo hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Kisha aichune hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima na kuichangua. Kisha wana wa Haroni walio watambikaji watie moto hapo pa kutambikia na kupanga kuni juu ya moto. Kisha wana wa Haroni walio watambikaji na wavipange vile vipande vya nyama, hata kichwa na mafuta juu ya kuni zilizopangwa juu ya moto uliowashwa mezani pa kutambikia. Lakini matumbo na miguu yake na aioshe kwa maji, kisha mtambikaji atayachoma moto yote yaliyowekwa juu ya meza ya kutambikia. Ndivyo, ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima inavyotolewa, iwe moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Kama toleo lake, analolitoa kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ni nyama mdogo kama kondoo au mbuzi sharti apeleke dume asiye na kilema. Amchinje mbele ya Bwana kando ya meza ya kutambikia upande wake wa kaskazini, nayo damu yake wana wa Haroni walio watambikaji na wainyunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia. Kisha amchangue, naye mtambikaji avipange vipande vyake pamoja na kichwa chake na mafuta yake juu ya moto uliowashwa mezani pa kutambikia. Lakini matumbo na miguu na aioshe kwa maji, kisha mtambikaji atayatoa yote kwa kuyachoma moto yote yaliyowekwa juu ya meza ya kutambikia. Ndivyo, naye nyama mdogo anavyokuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Kama toleo lake, analomtolea Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ni ndege, basi, sharti apeleke hua au kinda la njiwa manga. Naye mtambikaji atampeleka mezani pa kutambikia, atamvunja kichwa chake, apate kumchoma moto mezani pa kutambikia, lakini damu yake sharti idondoke ukutani pake meza ya kutambikia. Kisha akiondoe kibofu chake cha koo pamoja na machafu yaliyomo, akitupe majivuni kando ya meza ya kutambikia upande wa maawioni kwa jua. Kisha ampasue kidogo mabawani, lakini asiyatenge! Kisha mtambikaji amchome moto mezani pa kutambikia juu ya kuni zilizowekwa juu ya moto. Ndivyo, naye ndege anavyokuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Mtu akimpelekea Bwana toleo la vilaji vya tambiko sharti hilo toleo lake liwe unga mwembamba sana, alioumiminia mafuta na kuweka uvumba juu yake. Kisha aupeleke kwa wana wa Haroni walio watambikaji; ndipo, mtambikaji atakapochukua katika huo unga mwembamba wa kulijaza gao lake pamoja na mafuta, lakini uvumba atauchukua wote, kisha atauvukiza mezani pa kutambikia, uwe wa kumkumbushia Bwna, maana ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Lakini masao ya vilaji vya tambiko ni yao Haroni na wanawe, ndiyo matakatifu yenyewe yatokayo kwenye mioto ya Bwana. Lakini ukipeleka toleo la vilaji vya tambiko vilivyookwa jikoni, liwe la vikate vilivyotengenezwa pasipo chachu kwa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta au la maandazi yasiyochachwa yaliyopakwa mafuta. Lakini kama toleo lako ni vilaji vya tambiko vilivyokaangwa, liwe la maandazi yaliyotengenezwa pasipo chachu kwa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta; nawe uyakatekate vipande, kisha uvimiminie mafuta; ndivyo, vitakavyokuwa vilaji vya tambiko. Lakini kama toleo lako ni vilaji vya tambiko vilivyookwa katika chungu, na vitengenezwe kwa unga mwembamba na kutiwa mafuta. Ukitaka kumtolea Bwana vilaji vya tambiko vilivyotengenezwa hivyo, uvipeleke kwa mtambikaji, naye ataviweka mezani pa kutambikia. Kisha humo katika hivyo vilaji mtambikaji atanyanyua vingine, viwe vya kumkumbushia Bwana, atavivukiza mezani pa kumtambikia; ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Navyo vilaji vya tambiko vitakavyosalia vitakuwa vyao Haroni na wanawe, ndivyo vitakatifu vyenyewe, vitokavyo kwenye mioto ya Bwana. Vilaji vyote vya tambiko, mtakavyomtolea Bwana, visitengenezwe na kuchachwa. Kwani yote yaliyo yenye chachu au asali msiyavukize kuwa moto wa Bwana. Yakiwa ni matoleo ya malimbuko, basi, nayo mtamtolea Bwana, lakini penye meza ya kutambikia yasifike juu yake kuwa mnuko wa kumpendeza. Vilaji vyote vya tambiko, utakavyovitoa, uvitie chumvi, usiache kabisa, vilaji vyako vya tambiko vikose chumvi ya agano la Mungu wako, ila vilaji vyako vyote vya tambiko uvitoe, vikiwa vyenye chumvi. Lakini ukimtolea Bwana vilaji vya tambiko vya malimbuko, yawe masuke yaliyochomwa moto au chenga za ngano mpya, basi, hayo utayatoa kuwa vilaji vya tambiko vya malimbuko. Utayatia hata mafuta, kisha utaweka uvumba juu yao; ndivyo, yatakavyokuwa vilaji vya tambiko. Humo katika hizo chenga na yale mafuta mtambikaji atachukua mengine pamoja na uvumba wote, ayavukize yote, yawe ya kumkumbushia Bwana, maana ndio moto wa Bwana. Kama toleo lake ni ng'ombe ya tambiko ya shukrani, aliyoitoa katika ng'ombe wake, kama ni wa kiume au wa kike, sharti apeleke asiye na kilema, apate kumtoa mbele ya Bwana. Kisha aubandike mkono wake kichwani pake toleo lake, amchinje hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, nayo damu wana wa Haroni walio watambikaji na wainyunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia. Kisha na atoe katika huyo ng'ombe aliyechinjwa kuwa ng'ombe ya tambiko ya shukrani vile vipande vya kumchomea Bwana kwa moto, ni mafuta yanayoufunika utumbo pamoja na mafuta yote yanayoshikamana na utumbo, tena mafigo yake mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo penye nyama za viuno na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo; basi, haya yote na ayaondoe. Kisha wana wa Haroni na wayachome moto mezani pa kutambikia juu ya ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima iliyowekwa juu ya kuni zilizopangwa motoni; huu ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Lakini kama ng'ombe yake ya tambiko, anayotaka kumtolea Bwana, ameitoa katika mbuzi au kondoo, kama ni wa kiume au wa kike, sharti apeleke asiye na kilema. Kama anapeleka kondoo kuwa toleo lake, sharti ampeleke kumtoa mbele ya Bwana. Kisha aubandike mkono wake kichwani pake toleo lake, amchinje mbele ya Hema la Mkutano, nayo damu yake wana wa Haroni na wainyunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia. Kisha na atoe katika kondoo aliyechinjwa kuwa ng'ombe ya tambiko ya shukrani vile vipande vya kumchomea Bwana kwa moto, ni mafuta yake: mkia wenye mafuta, wote mzima auondoe kwa kuukata hapo, ulipoungwa na mifupa ya mgongoni, tena yale mafuta yanayoufunika utumbo pamoja na mafuta yote yanayoshikamana na utumbo, tena mafigo yake mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo penye nyama za viuno na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo; basi, haya yote na ayaondoe. Kisha mtambikaji na ayachome moto mezani pa kutambikia; hivyo yatakuwa vilaji vya moto wa Bwana. Lakini kama toleo lake ni mbuzi, sharti ampeleke kumtoa mbele ya Bwana. Kisha aubandike mkono wake kichwani pake, amchinje mbele ya Hema la Mkutano, nayo damu yake wana wa Haroni na wainyunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia. Kisha na atoe katika hilo toleo lake vile vipande vya kumchomea Bwana kwa moto: mafuta yanayoufunika utumbo pamoja na mafuta yote yanayoshikamana na utumbo, tena mafigo yake mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo penye nyama za viuno na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo; basi, haya yote na ayaondoe. Kisha mtambikaji na ayachome moto mezani pa kutambikia; hivyo yatakuwa vilaji vya moto vyenye mnuko unaopendeza. Mafuta yote ni yake Bwana. Huu ndio mwiko wa vizazi vyenu wa kale na kale mahali po pote, mtakapokaa: msile mafuta yo yote wala damu yo yote! Bwana akamwambia Mose kwamba: Waambie wana wa Isiraeli kwamba: Mtu akikosea agizo lo lote la Bwana asilikosee kwa kusudi, akifanya yasiyofanywa, ingawa ayafanye mara moja tu, na afanye hivyo: Mtambikaji aliyepakwa mafuta akiwaponza watu hawa, wakore manza kwa ajili ya kukosa kwake, basi, kwa ajili ya hilo kosa lake, alilolikosa, na apeleke dume la ng'ombe aliye mwana bado, asiye na kilema, wa kumtolea Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. Huyo dume atakapomfikisha mbele ya Bwana pa kuliingilia Hema la Mkutano au aubandike mkono wake kichwani pake huyo dume, kisha amchinje huyo dume mbele ya Bwana. Naye mtambikaji aliyepakwa mafuta na atwae damu nyingine ya huyo dume na kuiingiza Hemani mwa Mkutano. Kisha mtambikaji na achovye kidole chake katika damu, anyunyize damu kidogo mara saba mbele ya Bwana penye lile pazia la kupakingia Patakatifu. Kisha pembe zile za meza ya kumvukizia Bwana manukato iliyomo Hemani mwa Mkutano mtambikaji na azipake damu. Damu nyingine yote ya huyo dume aimwagie misingi ya meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko iliyopo hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Mafuta yote ya huyu dume aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo sharti ayaondoe kwake, ni yale mafuta yanayoufunika utumbo pamoja na mafuta yote yanayoshikamana na utumbo, tena mafigo yake mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo penye nyama za viuno na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo; basi, haya yote na ayaondoe. Kama anavyoyanyanyua katika ng'ombe aliyechinjwa kuwa ng'ombe ya tambiko ya shukrani, ndivyo, mtambikaji ayachome moto mezani pa kuteketezea ng'ombe za tambiko. Nayo ngozi ya huyu dume na nyama zake pamoja na kichwa chake na miguu yake na utumbo wake na mavi yake, haya yote pia ya huyu dume sharti ayatoe nje ya makambi na kuyapeleka mahali panapotakata, wanapomwagia majivu ya mafuta; ndipo ayaweke juu ya kuni, ayateketeze moto. Sharti yateketezwe papo hapo, wanapomwagia majivu ya mafuta. Mkutano wote wa Waisiraeli wakikosa neno, isipokuwa kwa kusudi, nalo hilo neno halikujulikana machoni pao wote, ya kuwa wamelikosea agizo moja tu katika maagizo yote ya Bwana wakifanya yasiyofanywa, basi, kama wamekora manza hivyo, hapo kosa lao, walilolikosa, litakapojulikana, wao wa mkutano na watoe dume la ng'ombe aliye mwana bado kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, wamfikishe mbele ya Hema la Mkutano. Kisha wazee wa mkutano na waibandike mikono yao kichwni pake huyo dume mbele ya Bwana, kisha wamchinje huyo dume mbele ya Bwana. Kisha mtambikaji aliyepakwa mafuta na aiingize damu nyingine ya huyo dume Hemani mwa Mkutano. Kisha mtambikaji na achovye kidole chake katika damu, anyunyize mara saba mbele ya Bwana penye lile pazia la kupakingia Patakatifu. Kisha pembe zile za meza ya Bwana iliyomo Hemani mwa Mkutano mbele ya Bwana na azipake damu, damu nyingine yote aimwagie misingi ya meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko iliyopo hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Mafuta yake yote sharti ayaondoe kwake, ayachome moto hapo mezani pa kutambikia, akimfanyizia huyu dume, kama anavyomfanyizia dume mwingine aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo; hivyo ndivyo, amfanyizie huyu naye. Hivyo mtambikaji atawapatia upozi, waondolewe makosa yao. Kisha na amtoe huyo dume nje ya makambi, amteketeze, kama alivyomteketeza yule dume wa kwanza. Hivyo ndivyo, ng'ombe ya tambiko ya weuo wa mkutano wote inavyotolewa. Mkuu wa watu atakapokosea agizo lo lote la Bwana Mungu wake na kufanya tendo moja tu lisilofanywa, kama hakulifanya kwa kusudi, basi, akikora manza hivyo, au hapo kosa lake, alilolikosa, litakapojulikana kwake kuwa ni kosa, na apeleke dume la mbuzi asiye na kilema kuwa toleo lake. Kisha na aubandike mkono wake kichwani pake huyo dume, kisha amchinje mahali hapo, wanapochinja mbele ya Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima; hivyo naye atakuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. Kisha mtambikaji na atwae damu nyingine ya huyu ng'ombe ya tambiko ya weuo kwa kidole chake, azipake pembe za meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, nayo damu yake nyingine aimwagie misingi ya meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko. Nayo mafuta yake yote na ayachome moto mezani pa kutambikia kama mafuta ya ng'ombe ya tambiko ya shukrani. Ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi, aondolewe kosa lake. Lakini mtu aliye mtumtu tu katika nchi hii akikosa, asipokosea agizo la Bwana kwa kusudi, akifanya tendo moja tu lisilofanywa, basi, akikora manza hivyo, au hapo kosa lake, alilolikosa, litakapojulikana kwake kuwa ni kosa, na apeleke jike la mbuzi asiye na kilema kuwa toleo lake kwa ajili ya kosa lake, alilolikosa. Kisha na aubandike mkono wake kichwani pake huyo ng'ombe ya tambiko ya weuo, kisha amchinje huyo ng'ombe ya tambiko ya weuo mahali hapo, wanapochinja ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima. Kisha mtambikaji na atwae damu yake nyingine kwa kidole chake, azipake pembe za meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, nayo damu yake nyingine yote aimwagie misingi ya meza ya kutambikia. Nayo mafuta yake yote na ayaondoe, kama mafuta yanavyoondolewa katika ng'ombe ya tambiko ya shukrani. Kisha mtambikaji na ayachome moto mezani pa kutambikia, yawe mnuko wa kumpendeza Bwana. Ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi, aondolewe kosa lake. Lakini kama anapeleka kondoo, amtoe kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo sharti apeleke jike asiye na kilema. Kisha na aubandike mkono wake kichwani pake huyo ng'ombe ya tambiko ya weuo kisha amchinje huyo ng'ombe ya tambiko ya weuo mahali hapo, wanapochinja ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima. Kisha mtambikaji na atwae damu nyingine ya huyo ng'ombe ya tambiko ya weuo kwa kidole chake, azipake pembe za meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, nayo damu yake nyingine yote aimwagie misingi ya meza ya kutambikia. Nayo mafuta yake yote na ayaondoe, kama mafuta ya kondoo aliye ng'ombe ya tambiko ya shukrani yanavyoondolewa, kisha mtambikaji na ayachome moto mezani pa kutambikia juu ya mioto ya Bwana. Ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi, aondolewe kosa lake, alilolikosa. Tena mtu anaweza kukosa hivi: akisikia shaurini sauti ya mwenye kuapiza, naye ni shahidi kwa kuliona lile jambo au kwa kulijua, basi, asipolieleza, atakuwa amekora manza zitakazomkalia. Au hivi: mtu akigusa cho chote kisichotakata, kama ni mzoga wa nyama chafu wa porini au mzoga wa nyama chafu wa kufugwa au mzoga wa dudu chafu, asijue, ya kuwa amejipatia uchafu, basi, naye ni mwenye manza. Au hivi: mtu akigusa uchafu wo wote wa mtu au kichafu cho chote, basi, hapo atakapokijua atakuwa ni mwenye manza. Au hivi: mtu akiapa kwa upuzi wa midomo tu, kama ni kwamba kufanya mabaya au mema, kwa hayo yote, mtu anayoyaapa kwa kujipuza, asijue, ya kwamba amekosa, basi, hapo atakapoyajua atakuwa ni mwenye manza kwa kosa moja kama hilo kuliko mengine. Na viwe hivyo: mtu, aliyekora manza kwa kosa moja kama hilo kuliko mengine, na aungame aliyoyakosea, kisha ampelekee Bwana malipo ya manza zake, alizozikora kwa ajili ya kosa lake, alilolikosa, akitoa katika kundi lake jike la kondoo au la mbuzi kwa ajili ya kosa lake. Ndipo, mtambikaji atakapompatia upozi, aondolewe kosa lake. Lakini mkono wake usipomfikilia kondoo, na ampelekee Bwana hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga kuwa ng'ombe yake ya tambiko ya weuo kwa ajili ya hilo kosa, alilolikosa, mmoja wa weuo, mmoja wa kuteketezwa nzima. Akiwapeleka kwa mtambikaji, huyo atatoa kwanza yule wa weuo akivunja kichwa chake hapo, kinaposhikamana na shingo, lakini hatakiondoa kabisa. Nayo damu yake nyingine ya yule wa weuo atainyunyizia ukutani pake meza ya kutambikia, nyingine itakayosalia na imwagike misingini pake meza ya kutambikia. Hivyo ndivyo, anavyokuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. Yule wa pili atamfanya kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima kama desturi. Hivyo ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi, aondolewe kabisa kosa lake, alilolikosa. Lakini mkono wake usipowafikilia hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga, basi, toleo lake, atakalopeleka, kwa kuwa alikosa, na liwe vibaba viwili na nusu vya unga mwembamba kuwa kipaji chake cha tambiko cha weuo; asiumiminie mafuta, wala asitie uvumba juu yake, kwani ndio kipaji cha tambiko cha weuo. Akiupeleka kwa mtambikaji, huyo mtambikaji na achukue humo wa kulijaza gao lake, uwe wa kumkumbushia Bwana, akiuchoma moto hapo pa kutambikia juu ya mioto ya Bwana. Hivyo nao utakuwa kipaji cha tambiko cha weuo. Hivyo ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi kwa ajili ya kosa lake, alilolikosa kuliko mengine, aondolewe kabisa kosa lake; nao unga uliosalia utakuwa wake mtambikaji kama ule wa vilaji vya tambiko. Bwana akamwambia Mose kwamba: Mtu akilivunja Agano, akikosa kwa kuchukua kitu kilicho mali ya Bwana, asipovijua, na ampelekee Bwana ng'ombe yake ya tambiko ya upozi, akitoa katika kundi lake dume la kondoo asiye na kilema, unayemwona kuwa wa fedha mbili tatu zilizopimwa kwa kipimo cha Patakatifu; huyo atakuwa ng'ombe yake ya tambiko ya upozi. Kisha nazo mali za Patakatifu, alizozikosea kwa kuzichukua, atazilipa na kuongeza fungu la tano; zote ampe mtambikaji. Ndipo, mtambikaji atakapompatia upozi na kumtoa yule dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi, kisha ataondolewa kosa lake. Hata mtu akikosea agizo lo lote la Bwana, ijapo ni moja tu, kwa kufanya yasiyofanywa, asipovijua, naye atakuwa amekora manza, nao uovu wake utamkalia. Kwa hiyo na atoe katika kundi lake dume la kondoo asiye na kilema, unayemwona, ya kama anatosha kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi. Kisha ampeleke kwa mtambikaji, naye mtambikaji atampatia upozi kwa ajili ya kosa lake, alilolikosa pasipo kulijua kuwa ni kosa; naye akiwa hakuvijua kweli ataondolewa kosa lake. Basi, hii ni ng'ombe ya tambiko ya upozi, kwa maana manza, alizozikora, alizikora kwake Bwana. Bwana akamwambia Mose kwamba: Ikiwa, mtu akose na kumvunjia Bwana Agano akimdanganya mwenziwe kwa kuchukua amana au mengine, aliyoyaweka mkononi mwake, au akimwibia au akimwonea mwenziwe, au akiokota kitu kilichopotea na kuvibisha na kuapa kiapo cha uwongo, akiwa amekosa moja tu katika mambo haya, watu wanayoyakosa, basi, akiwa amekora manza kwa kukosa hivyo, sharti ayarudishe aliyoyakwiba nayo aliyojipatia kwa kumwonea mwenziwe, nazo amana zilizowekwa kwake, nacho kilichopotea alichokiokota, nayo yote, aliyoyachukua kwa kuapa kiapo cha uwongo, yote pia ayalipe swasawa, kama yalivyokuwa, kisha sharti aongeze fungu la tano. Sharti mpe yeye aliye mwenye mali hizo siku hiyo, atakapotoa ng'ombe yake ya tambiko ya upozi. Hiyo ng'ombe yake ya tambiko ya upozi ampelekee Bwana akitoa katika kundi lake dume la kondoo asiye na kilema, utakayemwona, ya kama anatosha kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi; huyo na ampeleke kwa mtambikaji. Naye mtambikaji atampatia upozi mbele ya Bwana; ndipo, atakapoondolewa kosa lake, alilolikosa kuliko mengine yote kwa kukora zile manza. Bwana akamwambia Mose: Umwagize Haroni nao wanawe kwamba: Haya ndiyo maongozi ya ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima: ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima sharti ikae hapo, ilipowashiwa moto juu ya meza ya kutambikia usiku kucha, nao moto wa mezani pa kutambikia sharti uangaliwe, uwake vivyo hivyo. Naye mtambikaji na avae vazi lake la ukonge, hata suruali za ukonge na avae mwilini wake, nayo majivu ya ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima yaliyopo hapo juu ya meza ya kutambikia ayazoe, ayaweke kando ya meza ya kutambikia. Kisha na ayavue mavazi yake na kuvaa mavazi mengine, ayaondoe yale majivu na kuyapeleka nje ya makambi mahali panapotakata. Nao moto ulioko juu ya meza ya kutambikia uangaliwe, uwake hapo vivyo hivyo, usizimike. Kila kunapokucha mtambikaji ateketeze kuni juu yake, kisha juu yao apange ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, nayo mafuta ya ng'ombe za tambiko za shukrani ayachome moto juu yake. Moto na uangaliwe, uwake pasipo kukoma mezani pa kutambikia, usizimike. Nayo haya ndiyo maongozi ya vilaji vya tambiko: wana wa Haroni na wavipeleke kumtolea Bwana hapo mbele ya meza ya kutambikia. Kisha atanyanyua katika unga mwembamba wa kilaji cha tambiko wa kulijaza gao lake pamoja na mafuta yake na uvumba wote ulioko juu ya kilaji cha tambiko, auvukize mezani pa kutambikia, uwe mnuko upendezao wa kumkumbushia Bwana. Nao unga utakaosalia wataula Haroni na wanawe, uliwe hapo mahali patakatifu pasipo kutiwa chachu; waule uani penye Hema la Mkutano. Usiokwe ukiwa umechachuka. Kwani nimeutoa katika mioto yangu na kuwapa, uwe fungu lao, ndio mtakatifu mwenyewe kama ng'ombe ya tambiko ya weuo nayo ya upozi. Wana wa Haroni wote walio wa kiume wataula; hii na iwe haki ya kale na kale ya vizazi vyenu kuupata kwenye mioto ya Bwana. Kila atakayeugusa sharti awe ametolewa kuwa mtakatifu. Bwana akamwambia Mose kwamba: Hili ndilo toleo lao Haroni na wanawe, watakalomtolea Bwana siku hiyo, mmoja wao atakapopakwa mafuta: unga mwembamba pishi mbili na nusu na ziwe vilaji vyao vya tambiko vya kila siku nusu yao asubuhi, nusu yao nyingine jioni. Sharti uandaliwe kaangoni na kutiwa mafuta kuwa vitumbua. Kisha avipeleke na kuvimega vipandevipande; hivi ndivyo vilaji vya tambiko, utakavyovitoa, viwe mnuko wa kumpendeza Bwana. Mtambikaji aliyepakwa mafuta mahali pake Haroni miongoni mwa wanawe ndiye atakayevitoa; hii na iwe haki ya kale na kale ya Bwana, navyo sharti vichomwe moto vyote vizima. Kwani vilaji vya tambiko vyote, mtambikaji atakavyovitoa, sharti vichomwe moto vyote vizima, visiliwe. Bwana akamwambiaa Mose kwamba: Mwambie Haroni na wanawe: Haya ndiyo maongozi ya ng'ombe za tambiko za weuo: mahali hapo, ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima zinapochinjwa, nazo ng'ombe za tambiko za weuo zichinjwe papo hapo mbele ya Bwana, maana nazo ni takatifu zenywe. Mtambikaji atakayeitoa hiyo ng'ombe ya tambiko ya weuo ndiye atakayeila; sharti iliwe mahali patakatifu uani penye Hema la Mkutano. Kila atakayezigusa nyama zake sharti awe ametolewa kuwa mtakatifu. Tena kama iko damu yake iliyonyunyizika katika nguo, basi, hiyo nguo iliyonyunyizwa damu sharti aifue mahali patakatifu. Nacho chungu, nyama zake zilimopikwa, sharti kivunjwe; kama ni cha shaba, sharti kisuguliwe na kuoshwa kwa maji. Watambikaji wote walio wa kiume watazila nyama zake, nazo ni takatifu zenyewe. Lakini ng'ombe za tambiko za weuo zote, ambazo damu zao nyingine ziliingizwa Hemani mwa Mkutano, zitumiwe za upozi mle Patakatifu, nyama zao zisiliwe, ila ziteketezwe kwa moto. Nayo haya ndiyo maongozi ya ng'ombe za tambiko za upozi: ni takatifu zenyewe. Mahali hapo, wanapozichinja ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, papo hapo na wazichinje nazo ng'ombe za tambiko za upozi, nazo damu zao na azinunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia. Nayo mafuta yote ayatoe humo, ayapeleke: mkia na mafuta yanayoufunika utumbo, nayo mafigo yote mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo penye nyama za viuno na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo; basi, haya yote na ayaondoe. Kisha mtambikaji na ayachome moto mezani pa kutambikia kuwa moto wa Bwana. Hii ndiyo ng'ombe ya tambiko ya upozi. Watambikaji wote walio wa kiume na wazile nyama zake; nazo ziliwe mahali patakatifu, maana nazo ni takatifu zenyewe. Mambo ya ng'ombe za tambiko za weuo yalivyo, ndivyo, nayo ya ng'ombe za tambiko za upozi yalivyo, maongozi yao ni yayo hayo: nyama zitakuwa zake mtambikaji yule aliyempatia upozi mwenye ng'ombe. Naye mtambikaji akipeleka ng'ombe ya tambiko ya mtu ya kuteketezwa nzima, ngozi ya hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima itakuwa yake mtambikaji yule aliyeipeleka. Navyo vilaji vyote vya tambiko vinavyookwa jikoni, navyo vyote vilivyotengenezwa chunguni au kangoni vitakuwa vyake mtambikaji yule aliyevipeleka. Navyo vilaji vyote vya tambiko vilivyochanganywa na mafuta navyo vilivyo vikavu vitakuwa vyao wana wote wa Haroni, wavitumie kila mtu na ndugu yake. Haya ndiyo maongozi ya ng'ombe za tambiko za shukrani, mtu atakazomtolea Bwana: Mtu akiitoa kuwa ya sifa, na aitoe hiyo ng'ombe ya tambiko ya sifa pamoja na vikate visivyochachwa, vilivyochanganywa na mafuta, na unga mwembamba wa vitumbua wa kutengeneza vikate vilivyochanganywa na mafuta. Hili toleo lake alipeleke pamoja na mikate ilivyochachwa na pamoja na ng'ombe yake ya tambiko ya shukrani, atakayoitoa kuwa ya sifa. Katika hayo matoleo yote na atoe moja la kumnyanyulia Bwana; nalo ni lake mtambikaji yule atakayeinyunyiza damu ya ng'ombe ya tambiko ya shukrani. Nazo nyama za hiyo ng'ombe ya tambiko ya shukrani iliyo ya sifa na ziliwe siku hiyo ya kutolewa kwake, wasiziweke mpaka kesho. Akiitoa hiyo ng'ombe yake ya tambiko kwa ajili ya kiapo au kwa mapenzi yake mwenyewe, nyama zake hiyo ng'ombe ya tambiko na ziliwe siku hiyo ya kutolewa kwake, hata kesho yake masao yake yatalika. Lakini nyama za hiyo ng'ombe ya tambiko zitakazosazwa mpaka siku ya tatu sharti ziteketezwe kwa moto. Kama nyama za ng'ombe yake ya tambiko ya shukrani zingeliwa siku ya tatu, mwenye kuitoa asingependeza, wala asingewaziwa kuwa mwenye kuitoa, ila zitakuwa machukizo tu, naye kila mtu atakayezila atakuwa amekora manza. Nazo nyama zilizogusana nacho cho chote kilicho kichafu zisiliwe, ila ziteketezwe kwa moto. Nyama nyingine za tambiko kila atakataye atazila hizo nyama. Lakini kila mtu atakayekula nyama za ng'ombe ya tambiko ya shukrani zilizo zake Bwana, akiwa mwenye uchafu, basi, roho yake huyo mtu na ing'olewe, atoweke kwenye watu wa kabila lake. Tena mtu akigusa cho chote chenye uchafu, kama ni mtu aliye na uchafu wake au nyama chafu au tapisho lo lote linalochafua, naye akila nyama za ng'ombe ya tambiko ya shukrani zilizo zake Bwana, basi, roho yake huyo mtu na ing'olewe, atoweke kwenye watu wa kabila lake. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waambie wana wa Isiraeli kwamba: Mafuta yote ya ng'ombe na ya kondoo na ya mbuzi msiyale! Tena mafuta ya nyama aliyekufa kibudu nayo mafuta ya nyama aliyeraruliwa na nyama mwingine mtayatumia ya kazi yo yote, lakini kula msiyale! Kwani kila atakayekula mafuta ya nyama, watu wanayomtolea Bwana kuchomwa motoni, basi, roho yake huyo mtu aliyeyala na ing'olewe, atoweke kwenye watu wa kabila lake. Nazo damu zote pia msizile mahali po pote, mtakapokaa, wala za ndege wala za nyuma. Kila mtu atakayekula damu zo zote roho yake na ing'olewe, atoweke kwenye watu wa kabila lake. Bwana akamwambia Mose: Waambie wana wa Isiraeli kwamba: Atakayemtolea Bwana ng'ombe yake ya tambiko ya shukrani sharti ampelekee Bwana toleo lake, alilolitoa katika hiyo ng'ombe yake ya tambiko ya shukrani. Mikono yake mwenyewe na iyapeleke yatakayochomwa kwa moto wa Bwana, ni mafuta pamoja na kidari; akiyapeleka haya, kidari na wakipitishe motoni mbele ya Bwana, kiwe kipaji cha tambiko cha kupitishwa motoni. Kisha mtambikaji na ayachome moto yale mafuta mezani pa kutambikia, lakini kidari kitakuwa chao Haroni na wanawe. Nayo mapaja ya kuume ya ng'ombe zenu za tambiko za shukrani sharti mwape watambikaji kuwa vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa. Atakayetoa damu za ng'ombe za tambiko za shukrani pamoja na mafuta yao miongoni mwa wana wa Haroni, basi, lile paja la kuume ni fungu lake yeye, atakalolipata. Kwani vidari vya kupitishwa motoni na mapaja ya kunyanyuliwa ninayachukua kwa wana wa Isiraeli katika ng'ombe zao za tambiko za shukrani, nimpe mtambikaji Haroni na wanawe kuwa haki yao ya kale na kale kwao wana wa Isiraeli. Haya ndiyo, Haroni na wanawe watakayoyapata kwenye mioto ya Bwana kwa hivyo, walivyopakwa mafuta; Bwana aliwagawia haya siku ile, alipowatoa kuwa watambikaji wake. Siku ile, Bwana alipowapaka mafuta, aliwaagiza wana wa Isiraeli, wawape haya, nayo ni haki ya kale na kale ya vizazi vyao. Haya ndiyo malinganyo ya kutumia ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na vilaji vya tambiko na ng'ombe za tambiko za weuo na za upozi na za kujazwa gao nazo ng'ombe za tambiko za shukrani. Ndiyo, Bwana aliyomwagiza Mose mlimani kwa Sinai siku ile, alipowaagiza wana wa Isiraeli kumtolea Bwana matoleo yao katika nyika ya Sinai. Bwana akamwambia Mose kwamba: Mchukue Haroni pamoja na wanawe na yale mavazi na mafuta ya kupaka na dume la ng'ombe atakayekuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo na madume mawili ya kondoo na kikapu cha mikate isiyochachwa. Kisha ukusanye mkutano wote hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Mose akafanya, kama Bwana alivyomwagiza, nao mkutano ukakusanyika hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Mose akauambia mkutano: Hili ndilo, Bwana aliloliagiza kulifanya. Kisha Mose akamkaribisha Haroni nao wanawe, akawaosha kwa maji. Kisha akamvika shati, akaifunga kwa mkanda, akamvika kanzu, tena akamvika kisibau, akakifunga kwa masombo ya hicho kisibau na kukaza. Kisha akabandika hapo kibati, nacho hicho kibati akatia Urimu na Tumimu (Mwanga na Kweli). Kisha akamvika kilemba kichwani, nao upande wa mbele wa kilemba akabandika bamba la dhahabu, ndio ile taji takatifu, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha Mose akayatwaa yale mafuta ya kupaka, akalipaka lile Kao navyo vyote vilivyomo; ndivyo, alivyovieua. Nayo meza ya kutambikia akainyunyizia mafuta mara saba, akaipaka mafuta hiyo meza ya kutambikia na vyombo vyake vyote, hata birika na wekeo lake, avieue. Kisha akammiminia Haroni kichwani mafuta hayo ya kupakwa, akamweua kwa kumpaka mafuta hivyo. Kisha Mose akawakaribisha wana wa Haroni, akawavika shati, akazifunga kwa mikanda, akawavika vilemba virefu, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha akaagiza kumleta yule dume la ng'ombe ya tambiko ya weuo, naye Haroni na wanawe wakaibandika mikono yao kichwani pake yule dume la ng'ombe ya tambiko ya weuo. Kisha wakamchinja, naye Mose akatwaa damu, akaitia kwa kidole chake katika pembe za meza ya kutambikia pande zote, akaieua hiyo meza ya kutambikia, nayo damu nyingine akaimwagia misingi ya meza ya kutambikia, akaieua nayo, ajipatie upozi. Akayachukua mafuta yote yaliyoshikamana na utumbo na kile kipande cha ini na mafigo yote mawili pamoja na mafuta yao, kisha Mose akayachoma moto mezani pa kutambikia. Lakini yule dume la ng'ombe mwenyewe pamoja na ngozi yake na nyama zake na mavi yake akamteketeza kwa moto nje ya makambi, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha akamtoa dume la kondoo aliye ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, naye Haroni na wanawe wakaibandika mikono yao kichwani pake huyu dume la kondoo. Kisha Mose akamchinja, nayo damu akainyunyiza pande zote juu ya meza ya kutambikia. Kisha huyu dume la kondoo akachanguliwa vipande, naye Mose akamchoma moto, kichwa na vile vipande na mafuta; nao utumbo na miguu akaiosha kwa maji. Hivyo Mose akamchoma moto yule dume la kondoo wote mzima mezani pa kutambikia, awe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Ndivyo, alivyokuwa mnuko wa kupendeza, maana ni ng'ombe ya tambiko ya Bwana ya kuteketezwa kwa moto, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha akaagiza kuleta dume la kondoo wa pili aliye ng'ombe ya tambiko ya kujaza gao; naye Haroni na wanawe wakaibandika mikono yao kichwani pake huyo dume la kondoo. Kisha Mose akamchinja, akatwaa damu kidogo, akampaka Haroni pembe ya chini ya sikio lake la kuume na kidole gumba cha mkono wake wa kuume nacho cha mguu wake wa kuume. Kisha Mose akawakaribisha wanawe Haroni; nao akawapaka damu pembe za chini za masikio ya kuume na vidole gumba vya mikono yao ya kuume navyo vya miguu yao ya kuume, nayo damu nyingine Mose akainyunyizia misingi ya meza ya kutambikia pande zote. Kisha akayatwaa mafuta, ni mkia na mafuta yote yanayoshikamana na utumbo na kipande kile cha ini na mafigo yote mawili pamoja na mafuta yao na paja la kuume, tena katika kikapu cha mikate isiyochachwa kilichokuwa mbele ya Bwana akatwaa mkate mmoja usiochachwa na mkate mmoja wenye mafuta na andazi jembamba moja, akayaweka juu ya mafuta na juu ya paja la kuume. Kisha akayaweka yote pia mikononi mwa Haroni namo mikononi mwa wanawe, akayapitisha motoni mbele ya Bwana, yawe vipaji vya tambiko vya kupitishwa motoni. Kisha Mose akayatwaa tena mikononi mwao, akayachoma moto mezani pa kutambikia juu ya ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Hivyo ndivyo, ng'ombe za tambiko za kujaza gao zinavyotolewa, zipate kuwa mioto ya Bwana yenye mnuko wa kumpendeza. Kish Mose akakitwaa kidari cha yule dume la kondoo, akakipitisha motoni, kiwe kipaji cha tambiko cha kupitishwa motoni mbele ya Bwana; ndicho kipande cha ng'ombe ya tambiko ya kujaza gao kilichompasa Mose kuwa funga lake, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha Mose akatwaa mafuta kidogo ya kupaka na damu kidogo iliyokuwa mezani pa kutambikia, akamnyunyizia Haroni na mavazi yake nao wanawe na mavazi ya wanawe; ndivyo, alivyomweua Haroni na mavazi yake nao wanawe na mavazi yao pamoja naye. Kisha Mose akamwambia Haroni na wanawe: Zipikeni hizi nyama hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano! Tena hapo ndipo, mtakapozila pamoja na mikate iliyomo katika kikapu cha vilaji vya tambiko vya kujaza gao, kama nilivyoagizwa kwamba: Haroni na wanawe na waile! Masao ya nyama na ya mikate mtayateketeza kwa moto. Tena hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano msipatoke siku saba, mpaka siku zenu zilizowekwa za kutoa ng'ombe za tambiko za kujaza gao zitakapotimia, kwani siku za kujaza gao ni saba. Kama ilivyofanyika siku hii ya leo, ndivyo, Bwana alivyoagiza kufanya, mpatiwe upozi. Napo hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano mtakaa siku saba mchana kutwa na usiku kucha, mwulinde ulinzi wa Bwana, msife, kwani hivyo ndivyo, nilivyoagizwa. Naye Haroni na wanawe wakayafanya haya maneno yote, Bwana aliyoyaagiza kinywani mwa Mose. Siku ya nane Mose akamwita Haroni nao wanawe na wazee wa Isiraeli, akamwambia Haroni: Jichukulie ndama dume, awe ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena dume la kondoo, awe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, wote wawili wawe pasipo kilema, uwatoe mbele ya Bwana. Nao wana wa Isiraeli waambie kwamba: Chukueni dume la mbuzi, awe ng'ombe za tambiko ya weuo, tena ndama na mwana kondoo wa mwaka mmoja wasio na kilema, wawe ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima. Tena chukueni dume la ng'ombe na la kondoo, wawe ng'ombe z tambiko za shukrani wa kuwachinja mbele ya Bwana na vilaji vya tambiko vilivyochanganywa na mafuta. Kwani leo Bwana atawatokea ninyi. Wakayachukua yote, Mose aliyowaagiza, wakayapeleka hapo mbele ya Hema la Mkutano; nao mkutano wote ulipokuja, wakasimama mbele ya Bwana. Mose akasema: Hili ndilo neno, Bwana aliloliagiza, mlifanye, utukufu wa Bwana uwatokee. Kisha Mose akamwambia Haroni: Ikaribie meza ya kutambikia, utengeneze ng'ombe yako ya tambiko ya weuo nayo ya kuteketezwa nzima, ujipatie upozi mwenyewe! Tena kwa ajili ya watu nao litengeneze nalo toleo lao hawa watu, uwapatie upozi nao, kama Bwana alivyoyaagiza! Ndipo, Haroni alipoikaribia meza ya kutambikia, akamchinja ndama wake wa kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. Nao wanawe Haroni wakampelekea hiyo damu, naye akakichovya kidole chake katika damu, akazipaka pembe za meza ya kutambikia, nayo damu nyingine akaimwagia misingi ya meza ya kutambikia. Nayo mafuta na mafigo na kile kipande cha ini cha hiyo ng'ombe ya tambiko ya weuo akayachoma moto mezani pa kutambikia, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Nazo nyama na ngozi akaziteketeza kwa moto nje ya makambi. Tena alipomchinja ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, wanawe Haroni wakampelekea hiyo damu, naye akainyunyiza pande zote juu ya meza ya kutambikia. Hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ilipokwisha kuchanguliwa, wakampelekea vipande vyake pamoja na kichwa, naye akavichoma moto mezani pa kutambikia. Alipokwisha kuuosha utumbo na miguu akaichoma moto juu ya hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima mezani pa kutambikia. Kisha akayatoa matoleo ya watu. Akamchukua dume la mbuzi aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo ya watu, akamchinja na kumtoa kama yule wa kwanza, awe ng'ombe ya tambiko ya weuo. Akaitoa nayo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, akaifanya kama desturi. Alipovitoa vilaji vya tambiko akalijaza gao lake humo, akavichoma moto mezani pa kutambikia penye ng'ombe ya tambiko ya asubuhi ya kuteketezwa nzima. Kisha akamchinja dume la ng'ombe na dume la kondoo walio ng'ombe za tambiko za shukrani za watu, nao wanawe Haroni wakampelekea hizo damu, akazinyunyiza pande zote juu ya meza ya kutambikia. Nayo mafuta ya dume la ng'ombe, nayo ya dume la kondoo: mkia nayo yaufunikayo utumbo na mafigo na kile kipande cha ini, haya mafuta wakayaweka juu ya vidari, naye Haroni akayachoma moto haya mafuta mezani pa kutambikia. Lakini kidari na paja la kuume Haroni akavipitisha motoni huku na huko kuwa vipaji vya tambiko vya kupitishwa motoni mbele ya Bwana, kama Mose alivyoagiza. Kisha Haroni akawainulia watu mikono yake, akawabariki. Alipokwisha akashuka na kutoka hapo, alipozitoa ng'ombe za tambiko za weuo na za kuteketezwa nzima na za shukrani. Kisha Mose na Haroni wakaingia Hemani mwa Mkutano; napo walipotoka wakawabariki hao watu, ndipo, utukufu wa Bwana ulipowatokea watu wote. Moto ukatoka mbele ya Bwana, ukaila juu ya meza ya kutambikia ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima pamoja na yale mafuta. Watu wote walipoviona wakapiga shangwe na kuanguka kifudifudi. Wana wa Haroni, Nadabu na Abihu, wakachukua kila mtu chetezo chake, wakavitia moto, wakaweka mavukizo juu yake, wakamtolea Bwana moto huu mgeni, Bwana asiowaagiza. Ndipo, moto ulipotoka mbele ya Bwana, ukawala; ndivyo, walivyokufa mbele ya Bwana. Ndipo, Mose alipomwambia Haroni: Haya ndiyo, Bwana aliyoyasema kwamba: Nitajikatasa kwao, nitukuke mbele ya watu wote wa ukoo huu. Naye Haroni akanyamaza kimya. Kisha Mose akamwita Misaeli na Elsafani, wanawe Uzieli aliyekuwa baba mdogo wa Haroni, akawaambia: Njoni, mwachukue ndugu zenu na kuwaondoa hapa Patakatifu, mwapeleke nje ya malago. Wakaja, wakawachukua kwa shati zao na kuwapeleka nje ya malago, kama Mose alivyosema. Kisha Mose akamwambia Haroni na wanawe Elazari na Itamari: Nywele zenu za vichwani msiziache wazi, wala mavazi yenu msiyararue, msife, Bwana asiukasirikie mkutano wote. Ndugu zenu, wao wote walio wa mlango wa Isiraeli, na waomboleze kwa hivyo, walivyoteketezwa, Bwana mwenyewe akiwateketeza. Lakini ninyi msitoke hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, msife! Kwani mmekwisha kupakwa mafuta ya Bwana. Nao wakafanya, kama Mose alivyowaagiza. Bwana akamwambia Haroni kwamba: Mvinyo au kileo kingine usinywe wewe wala wanao, ulio nao, mkiingia Hemani mwa Mkutano, msife! Huu ndio mwiko wa kale na kale wa vizazi vyenu, mpate kuyapambanua yaliyo matakatifu nayo yaliyo ya watu wote, tena yaliyo machafu nayo yatakayo, mpate kuwafundisha hata wana wote wa Isiraeli maongozi yote, Bwana aliyowaambia kinywani mwa Mose. Mose akamwambia Haroni na wanawe Elazari na Itamari, ndio waliosalia: Twaeni vilaji vya tambiko vitakavyosalia penye moto wa Bwana, mvile hivyo visivyochachwa kando ya meza ya kutambikia! Kwani ndivyo vitakatifu vyenyewe. Mtavila mahali patakafifu, kwani ni haki yako na haki ya wanao kuvipata penye mioto ya Bwana, kwani nimeagizwa hivyo. Navyo vidari vilivyopitishwa motoni na mapaja yaliyonyanyuliwa hayo mtayala mahali panapotakata, wewe na wanao wa kiume na wa kike, kwani hii ni haki yako na ya wanao, yatolewe katika ng'ombe za tambiko za shukrani za wana wa Isiraeli, myapate. Mapaja ya kunyanyuliwa na vidari vya kupitishwa motoni kwanza wayapeleke hapo, mafuta yanapochomwa moto, wavipitishe motoni mbele ya Bwana hivyo vipaji vya tambiko vya kupitishwa motoni. Kuvipata hivi itakuwa haki yako na ya wanao ya kale na kale, kama Bwana alivyoagiza. Mose alipomtafuta sana dume la mbuzi aliyetolewa kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo aliona, ya kuwa amekwisha kuteketea; ndipo, alipowakasirikia wale wana wa Haroni waliosalia, Elazari na Itamari, akawaambia: Mbona hamkuila ng'ombe ya tambiko ya weuo mahali patakatifu? Kwani ndio takatifu yenyewe, nayo ndiyo, Bwana aliyowapa ninyi, mziondoe manza za mkutano na kuwapatia upozi mbele ya Bwana. Tazameni, damu yake haikupelekwa Patakatifu ndani ninyi iliwapasa kuila mahali patakatifu, kama nilivyoagiza. Haroni akamwambia Mose: Tazama, leo walipozitoa ng'ombe zao za tambiko za weuo na za kuteketezwa nzima mbele ya Bwana, yalinipata mambo kama hayo! Kama leo ningalikula ng'ombe ya tambiko ya weuo, sijui, kama ingalifaa machoni pake Bwana. Mose alipolisikia neno hili, likawa jema machoni pake. Bwana akasema na Mose na Haroni, akawaambia: Waambieni wana wa Israeli kwamba: Katika nyama wote walioko nchini mtakula hawa wenye miguu minne: wote wenye kwato zilizopasuka na kutengeka kabisa, kama ni wenye kucheua, mtawala. Lakini miongoni mwao wenye kucheua wapasukao kwato msiwale hawa: Ngamia; kweli anacheua, lakini hazipasui kwato zake vema, kwa hiyo ni mwiko kwenu. Pelele; naye anacheua, lakini hazipasui kwato, kwa hiyo ni mwiko kwenu. Sungura; naye anacheua, lakini hazipasui kwato, kwa hiyo ni mwiko kwenu. Nguruwe; kweli anazipasua kwato na kuzitenga kabisa, lakini hacheui, kwa hiyo ni mwiko kwenu. Nyama zao hao msizile, nayo mizoga yao msiiguse! kwani wao ni mwiko kwenu. Katika nyama wote waliomo majini mtakula hawa: wote wenye mapezi na magamba waliomo majini baharini na mitoni mtawala. Lakini wote wasio wenye mapezi na magamba waliomo baharini na mitoni miongoni mwao viumbe vyote vinavyotembea majini namo miongoni mwao nyama wote waliomo majini na wawe tapisho kwenu. Kweli na wawe tapisho kwenu! Nyama zao msizile, nayo mizoga yao na mwione kuwa tapisho; wote waliomo majini wasio wenye mapezi na magamba wawe tapisho kwenu. Namo katika ndege wamo, mtakaowaona kuwa tapisho, hawaliki kwa kuwa tapisho: kozi na pungu na furukombe, na tumbuzi na mwewe na ndugu zake, na makunguru yote na ndugu zao, na mbuni na kinega na dudumizi na kipanga na ndugu zake, na mumbi na shakwe na bundi, na yangeyange na korwa na tai, na korongo na kitwitwi na ndugu zake na hudihuda na popo. Wadudu wote wenye mabawa wanaokwenda kwa miguu minne wawe tapisho kwenu. Katika wadudu wote wenye mabawa wanaokwenda kwa miguu minne mtawala wao tu walio wenye miguu miwili mirefu ya kurukia nchini inayokaa penye miguu yao mingine juu kidogo. Mtakaowala miongoni mwao, ndio panzi na ndugu zao na nzige na ndugu zao na senene na ndugu zao na funutu na ndugu zao. Lakini wadudu wote wengine wenye mabawa wanaokwenda kwa miguu minne wawe tapisho kwenu. Kwao hao mtajipatia uchafu; kila atakayegusa mizoga yao atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye kila atakayechukua mzoga wao mmoja miongoni mwao sharti azifue nguo zake, naye atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Kila nyama mwenye kwato zilizopasuka pasipo kutengeka kabisa nao wasiocheua ndio walio wachafu kwenu; kila atakayewagusa atakuwa mwenye uchafu. Nao nyama wote wenye miguu minne wanaokanyaga kwa nyayo ndio walio wachafu kwenu; kila atakayegusa mizoga yao atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye atakayechukua mizoga yao sharti azifue nguo zake, naye atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Hao ndio walio wachafu kwenu. Tena katika nyama wadogo wanaotambaa juu ya nchi ndio hawa watakaokuwa wachafu kwenu: Fuko na panya ma mjusi na ndugu zao: guruguru na kenge na mbulu na goromoha na kinyonga. Hawa ndio walio wachafu kwenu katika nyama watambaao. Kila atakayewagusa wakiisha kufa atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Hata kila kitu, hawa watakachokiangukia wakifa, kitakuwa chenye uchafu kama ni chombo chochote cha mti au nguo au ngozi au gunia. Nacho kila chombo kinachotumiwa cha kufanyizia kazi kitiwe majini, nacho kitakuwa chenye uchafu mpaka jioni; ndipo, kitakapokuwa kimetakata tena. Lakini kila chombo cha udongo, ambacho mmoja wao ataanguka ndani yake, sharti wakivunje, nayo yote yaliyomo yatakuwa yenye uchafu. Vilaji vyote vinavyoliwa vikiingiwa na maji kama hayo ni vyenye uchafu; navyo vinywaji vyote vinavyonywewa vikiwa katika chombo kama hicho ni vyenye uchafu. Nacho cho chote, mzoga mmoja tu miongoni mwao utakachokiangukia, ni chenye uchafu; kama ni jiko la kuchomea mikate au la kupikia, sharti libomolewe, maana ni lenye uchafu, hata kwenu sharti liwe lenye uchafu. Lakini chemchemi na mashimo, maji yalimokusanyika, yatakuwa yametakata; lakini atakayeigusa mizoga yao akiyatoa humo atakuwa mwenye uchafu. Tena kama mzoga mmoja miongoni mwao utaangukia mbegu zo zote za kupanda, watu wanazotaka kuzipanda, zitakuwa zimetakata. Lakini kama mzoga mmoja miongoni mwao utaziangukia hizo mbegu, zikiisha lowekwa, sharti ziwe chafu kwenu. Tena mmoja wao hao nyama, mnaowala, akifa, atakayeugusa mzoga wake atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Atakayekula nyama ya mzoga wake sharti azifue nguo zake, tena atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye atakayeuchukua mzoga wake sharti azifue nguo zake, tena atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Nyama wadogo wanaotambaa juu ya nchi wote pia wawe tapisho kwenu, wasiliwe. Wote wanaojikokota tumboni nao wote wanaokwenda kwa miguu minne nao wote wenye miguu mingi zaidi, wale wadudu wote wanaotambaa juu ya nchi msiwale, kwani ndio tapisho. Msijifanye wenyewe kuwa tapisho kwa ajili ya hao wadudu watambaao, wala msijipatie uchafu kwa ajili yao mkichafuliwa nao. Kwani mimi ni Bwana, Mungu wenu, kwa hiyo sharti mjitakase, mwe watakatifu, kwani mimi ni mtakatifu. Msijipatie uchafu wenyewe kwao hao wadudu wote wanaotambaa juu ya nchi. Kwani mimi ndiye Bwana aliyewatoa ninyi katika nchi ya Misri na kuwapandisha kuja huku, niwe Mungu wenu; kwa hiyo sharti mwe watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu! Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya nyama na ya ndege na ya viumbe vyote vyenye uzima vinavyotembea majini na ya wadudu wote watambaao juu ya nchi, mpate kuwapambanua walio wachafu nao wanaotakata, ndio nyama wanaoliwa nao wasioliwa. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waambie wana wa Isiraeli kwamba: Mwanamke akipata mimba na kuzaa mtoto mume atakuwa mwenye uchafu siku saba, kama anavyokuwa mwenye uchafu siku zake za kuwa miezini. Siku ya nane mtoto na atahiriwe. Kisha huyo mwanamke na akae siku 33, damu yake ipate kutakata; cho chote kilicho kitakatifu asikiguse, wala asiingie Patakatifu, mpaka siku za weuo wake zitimie. Lakini akizaa mtoto mke atakuwa mwenye uchafu majuma mawili, kama vilivyo, akiwa miezini. Kisha atakaa siku 66, damu yake ipate kutakata. Siku za weuo wake kwa kuzaa mtoto mume au mke zitakapotimia, na apeleke mwana kondoo wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima na kinda la njiwa manga au hua kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo akiwafikisha hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano kwake mtambikaji. Naye atamtolea Bwana hizo ng'ombe za tambiko na kumpatia upozi; ndipo, atakapotakata kwa ajili ya hiyo damu yake iliyomtoka. Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya mwanamke aliyezaa mtoto mume au mke. Lakini mkono wake usipopata mwana kondoo na achukue hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga, mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, wa pili kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, mtambikaji ampatie upozi. Ndipo, atakapotakata. Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba: Ngozi ya mwili wa mtu ikitoa kivimbe au kipele au balanga, hiyo ngozi ya mwili wake ikitaka kumpatia pigo la ukoma, na apelekwe kwa mtambikaji Haroni au kwa mmoja wao wanawe walio watambikaji. Mtambikaji akilitazama hilo doa la ngozi ya mwili, akiona, ya kuwa nywele penye hilo doa zimegeuka kuwa nyeupe, tena hilo doa likionekana kuwa linabonyea katika ngozi nyingine ya mwili, basi, ndio doa la ukoma; mtambikaji akiisha kumwona kuwa hivyo hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu. Lakini hilo balanga jeupe penye ngozi ya mwili wake lisipoonekana, ya kuwa linabonyea katika ngozi, tena nywele zikiwa hazikugeuka kuwa nyeupe, mtambikaji atamfungia mwenye doa hilo siku saba. Siku ya saba mtambikaji atamtazama tena. Atakapoona kwa macho yake, ya kama hilo doa ni lilelile, ya kama hilo doa halikuongezeka katika ngozi, mtambikaji na amfungie mara ya pili siku saba. Mtambikaji akimtazama mara ya pili siku ya saba, akiona, ya kama hilo doa limo katika kufifia, ya kama hilo doa halikuongezeka katika ngozi, basi, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ametakata kwa kuwa ni mba tu, kisha mwenyewe na azifue nguo zake; ndipo, atakapokuwa ametakata. Lakini hiyo mba ikiongezeka katika ngozi, mtambikaji alipokwisha kumtazama na kusema, ya kuwa ametakata, sharti amtokee mtambikaji mara ya pili. Mtambikaji atakapomtazama tena na kuona, ya kama hiyo mba imeongezeka mwilini, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu, kwa kuwa ni ukoma. Mtu akiwa mwenye pigo la ukoma sharti apelekwe kwa mtambikaji. Mtambikaji akimtazama akiona kivimbe cheupe penye ngozi, akiona tena, ya kama hapo nywele zimegeuka kuwa nyeupe, akiona tena, ya kama nyama mbichi zimeota nyingi ndani ya kile kivimbe, basi, ndio ukoma wa kale hapo penye ngozi ya mwili wake, naye mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu pasipo kufungia, kwani ni mwenye uchafu kweli. Lakini ukoma ukitokea na kuenea katika ngozi po pote, ukoma ukiifunika hiyo ngozi iliyopatwa nao toka kichwani pake huyo mtu mpaka miguuni pake pote, macho ya mtambikaji yanapotazama, basi, mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama ukoma umeufunika mwili wake wote pia, hana budi kusema, ya kama mtu huyo aliyepatwa hivyo ni mwenye kutakata; kwa kugeuka wote mzima kuwa mweupe amekwisha kutakata. Lakini siku hiyo, nyama mbichi itakapoonekana kwake atakuwa mwenye uchafu. Naye mtambikaji akiiona hiyo nyama mbichi hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu; kwa kuwa hiyo nyama mbichi ni yenye uchafu, ndio ukoma. Lakini hiyo nyama mbichi ikigeuka tena kuwa nyeupe, na afike kwa mtambikaji. Mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama hapo palipopatwa na ukoma pamegeuka kuwa peupe, mtambikaji hana budi kusema, ya kama huyu aliyepatwa na ukoma ametakata, kwa kuwa amekwisha kutakata kweli. Mwili wa mtu ukiwa wenye jipu penye ngozi yake, nalo likipona, tena hapo, lile jipu lilipokuwa, pakitokea kivimbe cheupe au balanga jeupe lenye damudamu, sharti amtokee mtambikaji kutazamwa. Mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama hapo panaonekana kuwa panabonyea katika ngozi, tena ya kama nywele zimegeuka kuwa nyeupe, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu, ndio ugonjwa wa ukoma uliotokea hapo penye jipu. Lakini mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama nywele hazikugeuka kuwa nyeupe, tena hapakubonyea katika ngozi, ila panaanza kufifia, mtambikaji na amfungie siku saba. Basi, mahali pale pakiendelea katika ngozi, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu, kwani ndio ugonjwa ule mbaya. Lakini hilo balanga likiwa lilelile hapo mahali pake, lisiendelee, basi, ndio kovu la jipu tu, naye mtambikaji hana budi kusema, ya kama ametakata. Mwili wa mtu ukiwa wenye kidonda cha moto penye ngozi yake, nazo nyama za humo kidondani zikiwa balanga jeupe lenye damudamu au jeupe lenyewe, mtambikaji hana budi kupatazama; akiona, ya kama nywele zimegeuka kuwa nyeupe penye hilo balanga, napo pakionekana kuwa panabonyea katika ngozi, ndio ukoma uliotokea katika kidonda cha moto, naye mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu, kwani ndio ugonjwa wa ukoma. Lakini mtambikaji akipatazama na kuona, ya kama hapo penye balanga hapana nywele nyeupe, wala hapakubonyea katika ngozi, napo panaanza kufifia, mtambikaji na amfungie siku saba. Mtambikaji atakapomwona siku ya saba, ya kuwa mahali hapo pameendelea katika ngozi, mtambikaji hana budi kusema, ya kuwa ni mwenye uchafu, kwani ndio ugonjwa wa ukoma. Lakini kama hilo balanga ni lilelile mahali pake, halikuendelea katika ngozi, ila limeanza kufifia basi, ndio kivimbe cha kidonda cha moto tu, naye mtambikaji hana budi kusema, ya kama ametakata, kwani ni kovu tu la kidonda cha moto. Tena mtu mume au mke akitoka upele kichwani au kidevuni, mtambikaji akiutazama huo upele na kuona, ya kama unaonekana kuwa unabonyea katika ngozi, ya kama nazo nywele za hapo ni nyekundu kidogo, tena ni nyembamba, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu, kwani ndio upele mbaya, maana ukoma wa kichwani na wa kidevuni. Lakini mtambikaji akiutazama ugonjwa huo wa upele mbaya na kuona, ya kama hapaonekani kuwa panabonyea katika ngozi, tena ya kama hapana nywele zilizo nyekundu kidogo, mtambikaji na amfungie siku saba huyo mwenye ugonjwa wa upele mbaya. Mtambikaji atakapomtazama huyu mgonjwa siku ya saba na kuona, ya kama huo upele mbaya haukuendelea, wala hapana nywele zilizo nyekundu kidogo, wala upele huo mbaya hauonekani kuwa unabonyea katika ngozi, na ajinyoe nywele, lakini hapo penye upele mbaya asipanyoe; kisha mtambikaji na amfungie huyu mwenye upele mbaya mara ya pili siku saba. Mtambikaji atakapomtazama tena huyu mwenye upele mbaya siku ya saba na kuona, ya kama huo upele mbaya haukuendelea katika ngozi, wala hauonekani kuwa unabonyea katika ngozi, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ametakata, naye na azifue nguo zake, kisha atakuwa ametakata kweli. Lakini upele mbaya ukiendelea katika ngozi, mtambikaji alipokwisha kusema, ya kama ametakata, naye akimtazama tena na kuona, ya kama upele mbaya umeendelea katika ngozi, mtambikaji asitafute nywele zilizo nyekundu kidogo, kwani mtu yule ni mwenye uchafu. Lakini akiona kwa macho yake, ya kuwa upele mbaya ni uleule, ya kuwa nywele nyeusi zimeota hapo, basi, upele mbaya umepona, naye mwenyewe ametakata, naye mtambikaji hana budi kusema ya kama ametakata. Mtu mume au mke akiwa mwenye mabalanga penye ngozi ya mwili wake, hayo mabalanga yakiwa meupe, naye mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama penye ngozi ya mwili wake yako mabalanga meupe yaliyoanza kufifia, ndio mba zilizotoka katika ngozi, naye mwenyewe ni mwenye kutakata. Kama nywele za mtu zimeng'oka kichwani pake, ni mwenye kipara cha kisogoni, ni mwenye kutakata. Kama nywele za upande wa usoni zimeng'oka kichwani pake, ni mwenye kipara cha paji la usoni, naye ni mwenye kutakata. Lakini penye kipara cha kisogoni au cha utosini pakitokea vipele vyeupe vyenye damudamu, ndio ukoma unaotoka penye kipara chake cha kisogoni au cha utosini. Mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama ni kivimbe cha vipele vyeupe vyenye damudamu penye kipara chake cha kisogoni au cha utosini kinachoonekana kuwa kama ukoma penye ngozi ya mwili, basi, ni mtu mwenye ukoma, naye ni mwenye uchafu, naye mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu kweli, nao huo ugonjwa wake mbaya uko kichwani pake. Mwenye ukoma aliyepatwa na ugonjwa huu mbaya nguo zake sharti ziraruliwe, nazo nywele za kichwani pake sharti ziachwe wazi, nazo ndevu za midomoni sharti azifunike na kuita: Mchafu! Mchafu! Siku zote, atakazokuwa na ugonjwa huu mbaya atakuwa mwenye uchafu wa kweli, sharti akae peke yake, nalo kao lake sharti liwe nje ya makambi. Tena uko ukoma wa mavazi: vazi kama ni la nywele za kondoo au la pamba, linaweza kupatwa na ugonjwa huu mbaya wa ukoma; nguo yake ikiwa imefumwa au ikiwa imesokotwa na kushonwa, kama ni ya pamba au ya nywele za kondoo, kama ni ngozi yenyewe au ngozi iliyotengenezwa kwa namna yo yote, zote pia hupatwa na ukoma: madoadoa ya kimajanijani au ya damudamu yakitoka katika nguo au katika ngozi au katika nyuzi za kufumwa au katika nyuzi za kusokotwa au katika chombo cho chote kilichotengenezwa kwa ngozi, ndio huo ugonjwa mbaya wa ukoma; kwa hiyo sharti utazamwe na mtambikaji. Mtambikaji akiutazama huo ugonjwa mbaya, sharti hicho kilichopatwa nacho akifungie siku saba. Atakapokitazama siku ya saba hicho kilichopatwa na huu ugonjwa mbaya na kuona, ya kama ugonjwa huu mbaya umeendelea katika nguo au katika nyuzi za kufumwa au katika nyuzi za kusokotwa au katika ngozi, ijapo hiyo ngozi iwe imetengenezewa kazi yo yote, basi, ugonjwa huu mbaya ndio ukoma unaokula, nacho kile kitu ni chenye uchafu. Sharti waziteketeze hizo nguo au hizo nyuzi za kufumwa au hizo nyuzi za kusokotwa, kama ni za nywele za kondoo au za pamba, navyo vyo vyote vilivyotengenezwa kwa ngozi vilivyo vyenye ugonjwa huo mbaya, kwani ndio ukoma unaokula; kwa hiyo sharti viteketezwe kwa moto. Lakini mtambikaji akivitazama na kuona, ya kama ugonjwa huo mbaya haukuendelea katika nguo au katika nyuzi za kufumwa au katika nyuzi za kusokotwa au katika chombo cho chote cha ngozi, mtambikaji na aagize, wavifue vilivyo vyenye ugonjwa huo mbaya, kisha avifungie mara ya pili siku saba. Mtambikaji atakapovitazama vilivyopatwa na ugonjwa huo mbaya, vikiisha kufuliwa, na kuona, ya kama hapo penye ugonjwa huo mbaya hapakugeuka kuwa namna nyingine, ijapo ugonjwa wenyewe uwe haukuendelea, basi, ni vichafu, sharti waviteketeze kwa moto, kwani mahali hapo panabonyea upande wa nyuma na wa mbele. Lakini mtambikaji akipatazama na kuona, ya kama hapo penye ugonjwa huo mbaya pameanza kufifia, vile vitu vilipofuliwa, basi, na apaondoe katika nguo au katika ngozi au katika nyuzi za kufumwa au katika nyuzi za kusokotwa. Lakini ugonjwa huo ukionekana tena katika hizo nguo au katika hizo nyuzi za kufumwa au katika hizo nyuzi za kusokotwa au katika hivyo vyombo vyo vyote vya ngozi, kama unatokea humo tena, na wavichome moto vilivyopatwa na ugonjwa huo mbaya. Lakini hizo nguo au hizo nyuzi za kufumwa au hizo nyuzi za kusokotwa au hivyo vyombo vyo vyote vya ngozi vilivyotokwa na ugonjwa huo mbaya vilipofuliwa na vifuliwe mara ya pili; ndipo, vitakapokuwa vimetakata. Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya ugonjwa mbaya wa ukoma, ukishika nguo, kama ni za nywele za kondoo au za pamba, au nyuzi za kufumwa au nyuzi za kusokotwa au vyombo vyo vyote vya ngozi, wapate kusema, ya kama ni vyenye kutakata au vyenye uchafu. Bwana akamwambia Mose kwamba: Haya ndiyo maonyo yampasayo mtu mwenye ukoma siku ya kueuliwa kwake: sharti apelekwe kwa mtambikaji. Naye mtambikaji na amtokee nje ya makambi; mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama huyu mwenye ukoma amepona ugonjwa mbaya wa ukoma, mtambikaji na aagize, wamletee huyo mwenye kueuliwa ndege wawili walio wazima walio wenye kutakata, tena kipande cha mwangati na nyuzi nyekundu na kivumbasi. Kisha mtambikaji na aagize, ndege mmoja achinjwe juu ya mtungi wenye maji ya mtoni. Naye ndege wa pili aliye mzima na amshike pamoja na kile kipande cha mwangati na zile nyuzi nyekundu na kile kivumbasi, avichovye vyote pamoja na ndege aliye mzima katika damu ya ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni. Kisha amnyunyizie mara saba yule mwenye kueuliwa aliyepona ukoma. Akiisha kumweua hivyo na amwachilie huyo ndege aliye mzima, ajiendee maporini. Kisha mwenye kueuliwa na azifue nguo zake, tena na azinyoe nywele zake zote, hata koga na aoge majini. Ndipo, atakapokuwa ametakata. Baadaye ataweza kuingia makambini na kukaa siku saba nje penye hema lake. Siku ya saba na azinyoe nywele zake zote za kichwani pake na ndevu zake na nyushi za macho yake, nywele zake zote pia na azinyoe, nazo nguo zake na azifue, nao mwili wake auogeshe majini; ndipo, atakapokuwa ametakata. Siku ya nane na achukue wana kondoo wawili wasio na kilema na kondoo jike mmoja wa mwaka mmoja asiye na kilema na vibaba kumi vya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko na nusu kibaba ya mafuta. Kisha mtambikaji anayeeua na amsimamishe mwenye kueuliwa pamoja na hivyo vitu vyake mbele ya Bwana penye kuliingilia Hema la Mkutano. Kisha mtambikaji na achukue mwana kondoo mmoja, amtoe kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi pamoja na ile nusu kibaba ya mafuta, ampitishe motoni mbele ya Bwana kuwa kipaji cha tambiko cha kupitishwa motoni. Kisha na amchinje huyu mwana kondoo hapo mahali patakatifu, wanapochinja ng'ombe za tambiko za weuo nazo za kuteketezwa nzima. Kwani ng'ombe ya tambiko ya upozi ni yake mtambikaji kama ile ya weuo, ni takatifu yenyewe. Kisha mtambikaji na achukue damu kidogo ya ng'ombe ya tambiko ya upozi, yeye mtambikaji ampake mwenye kueuliwa pembe ya chini ya sikio lake la kuume na dole gumba la mkono wake wa kuume nalo dole gumba la mguu wake wa kuume. Kisha mtambikaji na achukue mafuta kidogo ya ile nusu kibaba, ayamimine katika gao lake mtambikaji la mkono wake wa kushoto. Kisha mtambikaji na akichovye kidole chake cha kuume katika mafuta yaliyomo katika gao lake la kushoto, ayanyunyize mara saba mafuta hayo kwa kidole chake mbele ya Bwana. Nayo mafuta yatakayosalia gaoni mwake mtambikaji mengine na ayatumie kumpaka mwenye kueuliwa pembe ya chini ya sikio lake la kuume na dole gumba la mkono wake wa kuume nalo dole gumba la mguu wake wa kuume juu ya damu ya ng'ombe ya tambiko ya upozi. Nayo mafuta mengine yatakayosalia gaoni mwake mtambikaji na ampake mwenye kueuliwa kichwani; ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi mbele ya Bwana. Kisha mtambikaji na aitengeneze ng'ombe ya tambiko ya weuo, ampatie huyo mwenye kueuliwa upozi, uchafu wake umtoke. Baadaye na aichinje ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Kisha mtambikaji na aitoe hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima pamoja na vilaji vya tambiko mezani pa kutambikia. Mtambikaji atakapokwisha kumpatia upozi hivyo, yule atakuwa ametakata. Lakini akiwa mkiwa, mkono wake usiyafikilie haya, basi, na achukue mwana kondoo mmoja tu kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi ya kupitishwa motoni, ajipatie upozi, na vibaba vitatu tu vya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko na nusu kibaba ya mafuta, tena hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga, kama mkono wake unavyoweza kufikilia, mmoja awe ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili awe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Siku ya nane akiisha kuambiwa, ya kama ni mwenye kutakata, awapeleke kwa mtambikaji hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, mbele ya Bwana. Naye mtambikaji na amchukue mwana kondoo aliye ng'ombe ya tambiko ya upozi pamoja na ile nusu kibaba ya mafuta, yeye mtambikaji ampitishe motoni mbele ya Bwana kuwa kipaji cha tambiko cha kupitishwa motoni. Kisha na amchinje huyu mwana kondoo aliye ng'ombe ya tambiko ya upozi, kisha mtambikaji na achukue damu kidogo ya hiyo ng'ombe ya tambiko ya upozi, ampake mwenye kueuliwa pembe ya chini ya sikio lake la kuume na dole gumba la mkono wake wa kuume nalo dole gumba la mguu wake wa kuume. Kisha mtambikaji na amimine mafuta kidogo katika gao lake mtambikaji la mkono wake wa kushoto. Kisha mtambikaji na anyunyize kwa kidole chake cha kuume mara saba mbele ya Bwana mafuta yaliyomo katika gao lake. Kisha mtambikaji hayo mafuta yaliyomo katika gao lake mengine na ayatumie kumpaka mwenye kueuliwa pembe ya chini ya sikio lake la kuume, nalo dole gumba la mkono wake wa kuume, nalo dole gumba la mguu wake wa kuume hapo penye damu ya ng'ombe ya tambiko ya upozi. Nayo mafuta mengine yatakayosalia gaoni mwake mtambikaji na ampake mwenye kueuliwa kichwani, ampatie upozi mbele ya Bwana. Kisha mtambikaji na atengeneze hua mmoja au kinda moja la njiwa manga, mkono wake yule ulioweza kuwatoa. Hawa, mkono wake yule ulioweza kuwatoa, mmoja awe ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili awe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima pamoja na vilaji vya tambiko; hivyo ndivyo, mtambikaji atakavyompatia mwenye kueuliwa upozi mbele ya Bwana. Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya mtu aliyepatwa na ugonjwa huo mbaya wa ukoma, ambaye mkono wake hauwezi kuyatoa yaupasayo weuo wake. Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba: Mtakapoiingia nchi ya Kanaani, nitakayowapa kuwa yenu, itakuwa, nipige nyumba ya hiyo nchi, ikiisha kuwa yenu, hiyo nyumba ipatwe na ukoma; ndipo mwenye nyumba na afike kwa mtambikaji kumpasha habari kwamba: Nyumbani mwangu mna kitu kinachoonekana kuwa kama ugonjwa mbaya. Naye mtambikaji na aagize, watoe humo nyumbani yaliyomo, yeye mtambikaji akiwa hajafika bado kuutazama huo ugonjwa mbaya, kusudi yote yaliyomo humo nyumbani yasipate kuwa yenye uchafu. Baadaye mtambikaji na aingie kuitazama hiyo nyumba. Akipatazama hapo palipopatwa na ugonjwa huo mbaya na kuona, ya kama ugonjwa huo mbaya umezipata kuta za hiyo nyumba na kutia vishimoshimo vyenye madoadoa ya kimajanijani au ya damudamu, navyo vikionekana kuwa vinabonyea ukutani, mtambikaji na atoke humo nyumbani na kupitia hapo pa kuiingilia nyumba hiyo, kisha hiyo nyumba na aifunge siku saba. Mtambikaji atakaporudi siku ya saba, akiitazama na kuona, ya kama huo ugonjwa mbaya umeendelea katika kuta za nyumba hiyo, mtambikaji na aagize, wayatoe hayo mawe yaliyopatwa na huo ugonjwa mbaya, wayatupie mahali penye uchafu nje ya mji. Kisha hiyo nyumba na waikwangue po pote upande wa ndani, nazo takataka, watakazokwangua, na wazimwage mahali penye uchafu nje ya mji. Kisha na wachukue mawe mengine, wayatie hapo, yale mawe yalipokuwa, kisha wachukue udongo mwingine wa kuipaka hiyo nyumba. Ugonjwa huo mbaya utakaporudi na kutokea tena humo nyumbani, wakiisha kuyatoa mawe yote na kuikwangua hiyo nyumba na kuipaka tena, mtambikaji sharti aje tena; akiitazama na kuona, ya kama ugonjwa huo mbaya umeendelea humo nyumbani, basi, ndio ukoma unaokula humo nyumbani, kwa hiyo nyumba ni yenye uchafu. Kwa sababu hii hawana budi kuibomoa hiyo nyumba, nayo mawe yake na miti yake na takataka zote za hiyo nyumba sharti wazipeleke nje ya mji na kuzitupia mahali penye uchafu. Naye atakayeingia humo nyumbani, siku zote ikiwa imefungwa, atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye atakayelala humo nyumbani sharti azifue nguo zake, naye atakayekula humo nyumbani sharti azifue nguo zake. Lakini mtambikaji akiingia humo na kutazama, basi, akiona, ya kama huo ugonjwa mbaya haukuendelea humo nyumbani, walipokwisha kuipaka tena, mtambikaji hana budi kusema, ya kama hiyo nyumba imekwisha kutakata, kwa kuwa ugonjwa huo mbaya umepona. Kisha na achukue ndege wawili na kipande cha mwangati na nyuzi nyekundu na kivumbasi. Ndege mmoja na amchinje juu ya mtungi wenye maji ya mtoni. Kisha na akichukue kile kipande cha mwangati na kile kivumbasi na hizo nyuzi nyekundu pamoja na yule ndege aliye mzima, vyote pamoja avichovye katika damu ya ndege aliyechinjwa, hata katika yale maji ya mtoni, kisha ainyunyizie hiyo nyumba mara saba. Ndivyo, atakavyoieua hiyo nyumba kwa damu ya ndege na kwa maji ya mtoni na kwa ndege aliye mzima na k kipande cha mwangati na kwa kivumbasi na kwa nyuzi nyekundu. Kisha na amwachilie yule ndege aliye mzima, ajiendee nje ya mji maporini. Ndivyo, atakavyoipatia hiyo nyumba upozi, ipate kuwa yenye kutakata. Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya kila namna ya ugonjwa huo mbaya wa ukoma na wa upele mbaya, hata wa ukoma wa nguo na wa nyumba na wa kivimbe na wa kipele na wa balanga, watu wapate kufundishwa siku za kuwa wenye uchafu nazo siku za kuwa wenye kutakata. Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya ukoma. Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba: Semeni na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Mtu mume ye yote akiwa mwenye kisonono mwilini mwake ni mwenye uchafu kwa ajili ya hicho kisonono chake. Nao uchafu, anaoupata kwa kisonono chake, ni wa namna hii: kama mwili wake unachuruzika usaha wa kisonono chake, au kama mwili wake unaukomeshakomesha, uchafu ni uo huo. Kilalo cho chote, mwenye kisonono atakachokilalia, ni chenye uchafu. Naye mtu atakayekigusa kilalo chake sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye atakayekalia kitu, mwenye kisonono alichokikalia, sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye atakayeugusa mwili wake mwenye kisonono sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye mwenye kisonono akitemea mate mwenye kutakata, huyo sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Nayo matandiko yo yote, mwenye kisonono atakayoyakalia akipanda, yatakuwa yenye uchafu. Naye kila atakayegusa cho chote kilichokuwa chini yake atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni, naye atakayevichukua vilivyo hivyo sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye kila mtu, mwenye kisonono atakayemgusa pasipo kunawa kwanza mikono yake kwa maji, sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Nacho chombo cha udongo, mwenye kisonono atakachokigusa, sharti kivunjwe, nacho kila chombo cha mti sharti kioshwe majini. Lakini mwenye kisonono akipata kutakata, kwa kuwa kisonono chake kimekoma, sharti ahesabu siku saba kuanzia hapo, alipopata kutakata, kisha sharti azifue nguo zake pamoja na koga katika maji ya mtoni; ndipo, atakapokuwa mwenye kutakata. Siku ya nane na achukue hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga, amtokee Bwana hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, ndipo ampe mtambikaji wale ndege. Naye mtambikaji na awatengeneze, mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi mbele ya Bwana kwa ajili ya kisonono chake. Lakini mtu akitokwa na mbegu akilala sharti auogeshe mwili wake wote mzima majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Nazo nguo zote na ngozi zote zilizonyewa na hizo mbegu sharti zifuliwe majini, nazo zitakuwa zenye uchafu mpaka jioni. Tena mtu aliye hivyo akilala na mwanamke, sharti wote wawili na waoge majini, kisha watakuwa wenye uchafu mpaka jioni. Mwanamke akiingia miezini, atokwe na damu mwilini mwake, sharti atengwe siku saba, naye kila atakayemgusa atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Nayo yote, atakayoyalalia siku hizo za kutengwa kwake, yatakuwa yenye uchafu; nayo yote, atakayoyakalia, yatakuwa yenye uchafu. Naye kila atakayekigusa kilalo chake sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye kila atakayegusa cho chote, alichokikalia, sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye atakayegusa cho chote kilichoko juu ya kilalo chake au juu ya kitu, alichokikalia, atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Tena mtu akilala naye, akiwa miezini, atakuwa mwenye uchafu siku saba, hata kilalo chake, atakachokilalia, kitakuwa chenye uchafu. Mwanamke akitoka damu zake siku nyingi zisizo zake za kuwa miezini, au kama anatoka damu kuzipita hizo siku za kuwa miezini, basi siku zote za kutoka damu ni mwenye uchafu; kama alivyo akiwa miezini, ndivyo, mwenye uchafu alivyo siku hizo nazo. Kilalo cho chote, atakachokilalia siku zote za kutoka damu zake, ni chenye uchafu, kama kilalo chake cha kuwa miezini kilivyo chenye uchafu; nacho kitu cho chote, atakachokikalia, ni chenye uchafu, kama kilivyo chenye uchafu siku zake za kuwa miezini. Naye kila atakayevigusa atakuwa mwenye uchafu, sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Lakini akipata kutakata, kwa kuwa damu yake imekoma, sharti ahesabu siku saba, halafu atakuwa ametakata. Siku ya nane na achukue hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga, awapeleke kwa mtambikaji penye kuliingilia Hema la Mkutano. Naye mtambikaji na atengeneze mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi mbele ya Bwana kwa ajili ya uchafu wake, damu zake ziliomtia. Hivi ndivyo, mtakavyowatengesha wana wa Isiraeli na uchafu wao, wasife kwa ajili ya uchafu wao wakilichafua Kao langu lililoko katikati yao. Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya mwenye kisonono nayo yake anayejipatia uchafu kwa kutokwa na mbegu akilala; tena ya mwanamke akiingia miezini, nayo ya kila mwenye kisonono, kama ni mtu mume, au kama ni mtu mke, nayo ya mtu anayelala na mwanamke aliye mwenye uchafu. Wale wana wawili wa Haroni walipouawa kwa kumtokea Bwana kwa njia isiyopasa, walipokwisha kufa, Bwana akasema na Mose; hapo Bwana alimwambia Mose: mwambie kaka yako Haroni, asiingie wakati wo wote Patakatifu ndani ya kile chumba cha mbele ya lile pazia na kukitokea Kiti cha Upozi kilichoko juu ya hilo Sanduku, asipate kufa. Kwani mimi hutokea winguni juu ya hicho Kiti cha Upozi. Ila Haroni apaingie Patakatifu akipeleka dume la ng'ombe aliye ndama bado kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo na dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Kuvaa na avae shati takatifu ya ukonge na suruali za ukonge mwilini mwake, nazo azifunge kwa mknda wa nguo y ukonge, tena na ajifunge kilemba cha ukonge, maana haya ndiyo mavazi yake matakatifu; kwanza sharti auogeshe mwili wake majini, kisha na ayavae hayo mavazi. Kisha na achukue kwa mkutano wa wana wa Isiraeli madume mawili ya mbuzi kuwa ng'ombe za tambiko za weuo na dume moja la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Kwanza Haroni na amtoe huyo dume la ng'ombe aliye ng'ombe yake ya tambiko ya weuo, ajipatie upozi mwenyewe nao wa mlango wake. Kisha na awachukue wale madume mawili ya mbuzi, awasimamishe mbele ya Bwana hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Kisha Haroni na awapigie kura hawa madume mawili, kura moja ya Bwana, ya pili ya Azazeli. Kisha Haroni na amtoe dume yule aliyeangukiwa na kura ya Bwana; huyu amtengeneze kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. Naye dume aliyeangukiwa na kura ya Azazeli na amsimamishe mbele ya Bwana, akiwa mzima, atumiwe kuwapatia upozi, wakimtuma kujiendea kwa Azazeli nyikani. Na viwe hivyo: Haroni akimtoa huyo dume la ng'ombe aliye ng'ombe yake ya tambiko ya weuo, ajipatie upozi mwenyewe nao wa mlango wake, na amchinje huyo dume la ng'ombe aliye ng'ombe yake ya tambiko ya weuo. Kisha na achukue chetezo kinachojaa makaa ya moto yatokayo mezani pa kutambikia mbele ya Bwana na magao mawili ya mavukizo yanukayo vizuri yaliyopondwa kuwa unga, aingie nayo katika chumba cha mbele ya lile pazia. Humo na ayatie hayo mavukizo juu ya moto mbele ya Bwana, moshi ya hayo mavukizo ukifunike Kiti cha Upozi kilichoko juu ya Sanduku la Ushahidi, asipate kufa. Kisha na achukue damu kidogo ya huyu dume la ng'ombe, ainyunyize kwa kidole chake juu ya Kiti cha Upozi upande wake wa maawioni kwa jua, napo mahali palipo mbele ya Kiti cha Upozi apanyunyizie mara saba hiyo damu kwa kidole chake. Kisha na amchinje yule dume la mbuzi aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo ya watu, damu yake nayo na aipeleke ndani ya chumba cha mbele ya lile pazia, kisha na aitumie hiyo damu kuyafanya yaleyale, aliyoyafanya kwa damu ya yule dume la ng'ombe, akiinyunyizia Kiti cha Upozi na mahali palipo mbele ya Kiti cha Upozi. Ndivyo, atakavyopapatia Patakatifu upozi, machafu ya wana wa Isiraeli na mapotovu yao yapatoke, maana makosa yao yote yamo. Kisha nalo Hema la Mkutano na alifanyizie vivyo hivyo, kwa kuwa linakaa nao katikati ya machafu yao. Mle Hemani mwa Mkutano msiwe na mtu ye yote, akiingia kupoza mle Patakatifu, mpaka atakapotoka akiisha kujipatia upozi mwenyewe nao wa mlango wake nao mkutano wote wa Waisiraeli. Akitoka na afike penye meza ya kutambikia iliyoko mbele ya Bwana, aipatie upozi nayo akichukua damu kidogo ya yule dume la ng'ombe na ya dume la mbuzi, azipake pembe za meza ya kutambikia pande zote. Kisha ainyunyizie damu kwa kidole chake mara saba, aieue na kuitakasa, machafu ya wana wa Isiraeli yaitoke. Akimaliza kupapatia upozi Patakatifu na Hema la Mkutano nayo meza ya kutambikia na amlete yule dume la mbuzi aliye mzima bado. Kisha Haroni na aibandike mikono yake yote miwili kichwani pake huyu dume la mbuzi aliye mzima bado, aungame juu yake manza zote za wana wa Isiraeli na mapotovu yao yote na makosa yao yote, ayatwike kichwani pake huyu dume la mbuzi, kisha na ampe mtu aliyewekwa kuwa tayari, ampeleke nyikani, ajiendee. Naye huyu dume la mbuzi na azichukue manza zao zote alizotwikwa, azipeleke katika nchi isiyokaa watu; huko nyikani ndiko amwachilie, ajiendee. Kisha Haroni sharti aingie Hemani mwa Mkutano kuzivua nguo zake za ukonge, alizozivaa alipoingia Patakatifu, aziweke hapo. Nao mwili wake sharti auogeshe majini mahali patakatifu, kisha na azivae nguo zake mwenyewe, kisha atoke, atengeneze ng'ombe yake ya tambiko ya kuteketezwa nzima nayo ya watu, ajipatie upozi mwenyewe, hata watu. Nayo mafuta ya ng'ombe ya tambiko ya weuo na ayateketeze kuwa moshi mezani pa kutambikia. Naye yule mtu aliyempeleka dume la mbuzi la Azazeli na kumwachilia sharti azifue nguo zake na kuuogesha mwili wake majini, baadaye ataweza kuingia makambini. Naye dume la ng'ombe aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo naye dume la mbuzi aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo, ambao damu zao zilipelekwa Patakatifi za kupozea mumo humo, na awapeleke nje ya makambi, wateketeze huko kwa moto ngozi zao na nyama zao na mavi yao. Naye atakayeziteketeza sharti azifue nguo zake na kuuogesha mwili wake majini, baadaye ataweza kuingia makambini. Haya na yawe kwenu maongozi ya kale na kale: katika mwezi wa saba siku ya kumi ya mwezi huu sharti mjitese wenyewe, msifanye kazi yo yote, wala wenyeji wala wageni walioko kwenu! Kwani siku hiyo ndipo, watakapowapatia upozi na kuwaeua, makosa yenu yote yawatoke, mpate kuwa wenye kutakata mbele ya Bwana. Siku hiyo ya mapumziko sharti iwe kwenu ya mapumziko kabisa; ndipo, mtakapojitesa kwa kufunga. Haya ndiyo maongozi ya kale na kale. Mwenye kupoza sharti awe mtambikaji, waliyempaka mafuta na kulijaza gao lake, apate kutambika mahali pa baba yake, naye sharti azivae hizo nguo za ukonge, maana ndizo nguo zipasazo Patakatifu. Kisha na apapatie upozi Patakatifu penyewe nalo Hema la Mkutano, nayo meza ya kutambikia na aipatie upozi, nao watambikaji wote pamoja na watu wote wa huu mkutano na awapatie upozi. Haya sharti yawe kwenu maongozi ya kale na kale ya kuwapatia upozi wana wa Isiraeli kila mwaka mara moja, makosa yao yote yawatoke. Naye akayafanya, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na Haroni na wana wote wa Isiraeli, uwaambie: Hili ni neno, aliloliagiza Bwana kwamba: Mtu ye yote wa mlango wa Isiraeli atkayechinja ng'ombe au kondoo au mbuzi makambini au atakayemchinja nje ya makambi, asimpeleke pa kuliingilia Hema la Mkutano, amtolee Bwana toleo la tambiko mbele ya Kao lake Bwana, mtu huyu na awaziwe kuwa mwenye manza za damu: kwa kuwa alimwaga damu, sharti ang'olewe mtu huyu katikati yao walio ukoo wake. Ni kwamba: ng'ombe zao za tambiko, wanazozichinja maporini, wana wa Isiraeli sharti wampelekee Bwana hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano na kumpa mtambikaji, ndipo wazichinje kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani za Bwana. Nazo damu mtambikaji na azinyunyize juu ya meza ya kumtambikia Bwana hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, nayo mafuta na ayateketeze kuwa moshi wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Ng'ombe zenu za tambiko msizitolee tena mashetani, mnaowwafuata kufanya ugoni nao. Haya sharti yawe kwao maongozi ya kale na kale ya kuongoza vizazi na vizazi vya kwao. Tena uwaambie: Mtu ye yote wa mlango wa Isiralei, hata mgeni atakayekaa kwao, atakayetoa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima au ng'ombe nyingine ya tambiko, asipoipeleka pa kuliingilia Hema la Mkutano kuiteketeza hapo, iwe ng'ombe ya tambiko ya Bwana, mtu huyu sharti ang'olewe kwao walio wa ukoo wake. Mtu ye yote wa mlango wa Isiraeli, hata mgeni atakayekaa kwao, atakayekula damu yo yote, mtu huyu atakayekula damu nitamkazia macho yangu, nimng'oe katikati yao walio ukoo wake. Kwani roho ya mwili imo katika damu, nami niliwapa damu, mzipeleke mezani pa kutambikia, ziwapatie upozi ninyi wenyewe, kwani damu humpatia mtu upozi, kwa kuwa roho imo. Kwa hiyo nimewaambia wana wa Isiraeli: Atakayekaa kwenu asile damu, wala mgeni atakayekaa kwenu asile damu! Mtu ye yote aliye wa wana wa Isiraeli naye mgeni atakayekaa kwao, akiwinda nyama au ndege anayelika, sharti aimwage damu yake na kuifunika kwa mchanga. Kwani roho ya kila mwenye mwili ni damu yake, maana humu ndimo, roho yake ilimo; kwa hiyo nimewaambia wana wa Isiraeli: Msile damu zao wo wote walio wenye miili! Kwani roho ya kila mwenye mwili ni damu yake, naye kila atakayeila sharti ang'olewe. Tena kila atakayekula kibudu au nyama aliyeraruliwa na nyama mwingine, kama ni mwenyeji au kama ni mgeni, sharti azifue nguo zake na koga majini, naye atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni, kisha atakuwa ametakata. Lakini asipozifua nguo zake, wala asipouogesha mwili wake majini, atakuwa amekora manza zitakazomkalia. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Mimi Bwana ni Mungu wenu. Msifanye matendo kama yale ya nchi ya Misri, mlikokaa, wala msifanye matendo kama yale ya nchi ya Kanaani, nitakakowapeleka kukaa huko, wala msiyafuate maongozi yao. Mtakapoyafanya maamuzi yangu na kuyaangalia maongozi yangu, myafuate, mimi Bwana nitakuwa Mungu wenu. Kwa hiyo yaangalieni maongozi yangu! Naye mtu ye yote atakayeyafanya maamuzi yangu atapata uzima kwa njia hiyo, maana mimi ni Bwana. Mtu ye yote asiingie kwa mwenziwe aliye ndugu yake wa kuzaliwa naye, amfunue uchi wake. Maana mimi ni Bwana. Uchi wa baba yako wala uchi wa mama yako usiufunue; aliye mama yako usimfunue uchi wake. Uchi wa mkewe baba yako usiufunue. Kwani ndio uchi wa baba yako. Uchi wa umbu lako aliye binti baba yako au binti mama yako, kama amezaliwa nyumbani mwenu au nje, usiufunue uchi wao hao. Uchi wa binti mwanao, wa kiume au wa kike, usifunue uchi wao hao, kwani ni uchi wako mwenyewe. Uchi wake binti mkewe baba yako, aliyezaliwa na baba yako, usiufunue huo uchi wake, maana ni umbu lako. Uchi wake umbu lake baba yako usiufunue, maana ni ndugu ya baba yako wa kuzaliwa naye. Uchi wa ndugu ya mama yako usiufunue. Kwani ni ndugu ya mama yako wa kuzaliwa naye. Uchi wa baba yako mkubwa au mdogo usiufunue, wala mkewe usimkaribie, maana ni mama yako. Uchi wa mkweo aliye mke wa mwanao wa kiume usiufunue huo uchi wake. Uchi wa mkewe mkubwa au mdogo wako usiufunue, maana ni uchi wa ndugu yako wa kuzaliwa naye. Uchi wa mwanamke usiufunue pamoja nao wa mwanawe wa kike. Wala usimchukue binti mwanawe wa kiume wala binti mwanawe wa kike kuufunua uchi wake. Maana hao wanawake ni ndugu wa kuzaliwa pamoja; huo ndio uzinzi. Wala usichukue mwanamke ukiwa na ndugu yake wa kike, umtie yule wivu kwa kuufunua uchi wake huyu siku zile, yule akiwa angaliko yu hai. Usimkaribie mwanamke aliye mwenye uchafu kwa kuwa miezini, uufunue uchi wake. Usiingie kwa mkewe mwenzako, ulale naye na kumpa mimba, usijipatie uchafu kwake. Namo miongoni mwao walio wa uzao wako usitoe hata mmoja wa kumpa Moloki, wamwingize motoni, usipate kulichafua Jina la Mungu wako. Mimi ni Bwana. Aliye wa kiume usilale naye, kama unavyolala na mwanamke, maana hayo ni matapisho. Wala usije kulala na nyama ye yote ukijipatia uchafu kwake, wala mwanamke asisimame mbele ya nyama kupata mimba kwake; huo ndio uchafu mbaya zaidi. Usijichafue kwa mambo hayo yote! Kwani kwa kuyafanya hayo yote walijichafua wamizimu wote, nitakaowafukuza mbele yenu. Kwa kuwa nchi ilipata kuwa yenye uchafu, nitailipisha huu uovu wake, iwatapike waliokuwa wenyeji huko. Lakini ninyi yaangalieni maongozi yangu na maamuzi yangu, msiyafanye hayo matapisho yote, wala ninyi mlio wenyeji wala wageni watakaokuwa kwenu. Kwani matapisho hayo yote waliyafanya wao waliokuwako mbele yenu katika nchi hiyo, hata nchi ikapata kuwa yenye uchafu. Nanyi mtakapoyafanya, nchi itawatapika kwa kuichafua, kama ilivyowatapika wamizimu waliokuwako mbele yenu. Kwani wote watakaoyafanya matapisho hayo, basi, wao watakaoyafanya watang'olewa kwao walio ukoo wao. Kwa hiyo yaangalieni, niliyowaambia, yanayowapasa kuyaangalia, msiyafuate na kuyafanya yale maongozi yatapishayo, yaliyofanywa mbele yenu, msijipatie uchafu kwa kuyafanya. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na mkutano wote wa wana wa Isiraeli, uwaambie: Sharti mwe watakatifu, kwani mimi Bwana Mungu wenu ni mtakatifu. Mtu sharti amche mama yake na baba yake. Nazo siku zangu za mapumziko sharti mziangalie. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Msivigeukie vinyago vilivyo vya bure, wala msijitengenezee miungu ya shaba au ya vinginevyo vilivyoyeyushwa. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Mtakapomtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya shukrani, sharti mwitoe hivyo, atakavyopendezwa nanyi. Siku ya kuitoa na iliwe, hata kesho yake; lakini nyama zitakazosalia mpaka siku ya tatu na ziteketezwe kwa moto. Lakini ikiliwa siku ya tatu, itachukiza, haitapendeza. Naye atakayeila atakuwa amekora manza, kwa kuwa ameichafua iliyo takatifu ya Bwana, kwa hiyo yeye mwenyewe atang'olewa kwao walio ukoo wake. Mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, msikate napo pembeni penye mashamba yenu kupavunia napo, wala msiokoteze viokotezo vya mavuno yenu. Wala usiipukuse mizabibu yako, wala zabibu zako zilizoanguka usiziokoteze, ila uziache, ziokotezwe na wakiwa na wageni. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Msiibe, wala msidanganywe, wala msiongopeane wenyewe na wenyewe. Msiape kiapo cha uwongo na kulitaja Jina langu. Maana hivyo utalichafua Jina la Mungu wako. Mimi ni Bwana. Usimkorofishe mwenzio na kumnyang'anya. Mshahara wa kazi, uliyofanyiziwa, usilale nao, mpaka kuche. Usiapize kiziwi, wala usiweke makwazo, kipofu anapopitia, ila umwogope Mungu wako! Mimi ni Bwana. Msifanye mapotovu mashaurini mkiupendelea uso wa mkiwa au mkimtukuza mkuu, ila umwamulie mwenzako kwa wongofu. usitembee kwa wenzako wa ukoo, upate mtu wa kumchongea. Usitoe ushahidi wa uwongo wa kumwua mwenzako. Mimi ni Bwana. Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Kuonya umwonye mwenzako, kusudi usijikoseshe kwa ajili yake. Usijilipize mwenyewe, wala usiwakasirikie wana wa ukoo wako, ila umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwwenyewe. Mimi ni Bwana. Yaangalieni maongozi yangu! Usiwaache nyama wako wa kufuga, walale pamoja na nyama wengine, wala shamba lako usilipande mbegu za namna mbili, wala mwilini mwako usivae nguo iliyofumwa kwa nyuzi za namna mbili. Mtu akilala kwa mwanamke kijakazi na kumpa mimba, naye alikuwa ameposwa na mtu mwingine, basi, akiwa hakukombolewa wala hakufunguliwa kujiendea, na wapatilizwe, lakini wasiuawe, kwa kuwa yule mwanamke hakufunguliwa kujiendea. Naye mume sharti apeleke dume la kondoo hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi ya kumtolea Bwana kwa ajili ya manza, alizozikora. Naye mtambikaji na ampatie upozi na kumtoa yule dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi mbele ya Bwana kwa ajili ya kosa lake, alilolikosa; ndipo, atakapoondolewa hilo kosa lake, alilolikosa. Mtakapoingia katika nchi ile mtapanda miti yo yote yenye matunda ya kula, lakini kwanza iacheni yenye magovi yao, ndio matunda yao, miaka mitatu mwiwazie kuwa haijatahiriwa, isiliwe. Katika mwaka wa nne matunda yao yote pia yawe matakatifu ya kumtolea Bwana shukrani. Katika mwaka wa tano mtaweza kuyala matunda yao; ndivyo, mtakavyojiongezea mapato yao. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Msile cho chote kilicho chenye damu bado. Msipige bao, wala msiagulie mawingu. Msichege nywele pembeni vichwani penu, wala ndevu zenu msizikate pembenipembeni. Msijichanje chale miilini mwenu kwa ajili ya wafu, wala msijiandike nembo miilini mwenu. Mimi ni Bwana. Mwanao wa kike usimtie uchafu na kumzinisha, hiyo nchi isipate kuwa yenye uzinzi, hiyo nchi ikijaa ugoni. siku zangu za mapumziko sharti mziangalie, napo Patakatifu pangu sharti mpache. Mimi ni Bwana. Msiwageukie waganga wa kutiisha mizimu wa waaguaji. Msiwatafute, mkajipatia uchafu kwao. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Mbele yake mwenye mvi sharti uinuke, naye aliye mzee sharti umheshimu usoni pake kwa kumwogopa Mungu wako. Mimi ni Bwana. Mgeni akikaa ugenini kwenu katika nchi yenu, msimwonee, ila awe kwenu kama mwenyeji, ijapo ni mgeni akaaye ugenini kwenu. Mmpende, kama mnavyojipenda; kwani nanyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Msifanye mapotovu wala mashaurini wala kwa kutumia vipimo vya kudanganya kama mizani au vibaba. Sharti mtumie mizani ya sawasawa na vyuma vya kupimia vya sawasawa na pishi za sawasawa na visaga vya sawasawa. Mimi Bwana ni Mungu wenu aliyewatoa katika nchi ya Misri. Yaangalieni maongozi yangu yote na maamuzi yangu, myafanye! Mimi ni Bwana. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waambie wana wa Isiraeli: Mtu ye yote, kama ni mwana wa Isiraeli au kama ni mgeni akaaye ugenini kwao Waisiraeli atakayetoa hata mmoja tu miongoni mwao walio wa uzao wake na kumpa Moloki sharti auawe, watu wa nchi hiyo sharti wamtupie mawe. Nami nitamkazia macho mtu aliye hivyo, nimng'oe katikati yao walio ukoo wake, kwani miongoni mwao walio wa uzao wake ametoa mtu wa kumpa Moloki, kusudi apapatie Patakatifu pangu uchafu, alibezeshe nalo Jina langu takatifu. Ijapo watu wa nchi hiyo wayapofushe macho yao, wakiyaona, mtu yule aliyoyafanya alipotoa mtu miongoni mwao walio wa uzao wake na kumpa Moloki, wasipate kumwua, mimi na nimkazie macho yangu mtu aliye hivyo nao walio wa kizazi chake, nimng'oe yeye pamoja nao wote waliomfuata na kuufanya ugoni wake wa kumfuata Moloki kufanya ugoni naye, basi, na niwang'oe, watoweke katikati yao walio ukoo wao. Hata mtu akiwageukia waganga wa kutiisha mizimu na waaguaji, kufanya ugoni nao, na nimkazie macho yangu aliye hivyo, na nimg'oe katikati yao walio ukoo wake. Kwa hiyo jitakaseni, mpate kuwa watakatifu! Kwani mimi Bwana ni Mungu wenu. Yaangalieni maongozi yangu, myafanye! Mimi ni Bwana anayewatakasa ninyi. Mtu ye yote atakayemwapiza baba yake au mama yake sharti auawe kabisa; akimwapiza baba yake au mama yake atakuwa amekora manza za kumwagwa damu yake. Mtu akizini na mke wa mwingine, basi, yeye aliyezini na mke wa mwenzake sharti auawe, mwenyewe pamoja na mwanamke, aliyezini naye. Mtu atakayelala na mkewe baba yake atakuwa ameufunua uchi wake baba yake; kwa hiyo wote wawili sharti wauawe, maana wamekora manza za kumwagwa damu zao. Mtu akilala na mke wa mwanawe, sharti wauawe wote wawili, maana wamefanya uchafu ulio mbaya zaidi, nao wamekora manza za kumwagwa damu zao. Mtu akilala na mwanamume mwingine, kama wanavyolala na mwnamke, wamefanya tapisho, wote wawili sharti wauawe, maaana wamekora manza za kumwagwa damu zao. Mtu akimchukua mwanamke pamoja na mama yake, ni ugoni, sharti wamteketeze kwa moto pamoja nao wale wanawake, ugoni ulio hivyo usiwe kwenu. Mtu akilala na nyama sharti auawe, hata huyo nyama sharti mmwue. Mwanamke akimkaribia nyama ye yote kulala naye, sharti mmwue huyo mwanamke pamoja na huyo nyama, wafe kabisa, maana wamekora manza za kumwagwa damu zao. Mtu akimchukua umbu lake aliye binti baba yake au binti mama yake, auone uchi wake, naye auone uchi wake yeye mwenyewe, ni tendo litwezalo, nao sharti wang'olewe machoni pao walio wana wa ukoo wao, maana ameufunua uchi wa umbu lake; hizi manza, alizozikora, zitamkalia. Mtu akilala na mwanamke aliye miezini, akiufunua uchi wake na kukitokeza waziwazi kijito chake, naye mwanamke akikifunua kijito cha damu yake, wote wawili sharti wang'olewe katikati yao walio ukoo wao. Uchi wa mama yako mkubwa na mdogo nao uchi wa shangazi yako usiufunue, kwani ni kuutokeza waziwazi uchi wao walio ndugu wa kuzaliwa nao; hizo manza, walizozikora, zitawakalia. Mtu akilala na mkewe baba yake mkubwa au mdogo, ameufunua uchi wa baba yake mkubwa au mdogo, nao huu ukosaji wao utawakalia, wafe pasipo kuzaa watoto. Mtu akimchukua mkewe mkubwa au mdogo wake, ni uchafu, maana ameufunua uchi wa ndugu yake wa kuzaliwa naye, nao watakufa pasipo kuzaa watoto. Yaangalieni maongozi yangu yote na maamuzi yangu yote, myafanye, ile nchi isiwatapike, nitakapowapeleka, mkae huko. Msiyafuate maongozi ya wamizimu, nitakaowafukuza mbele yenu. Kwa kuwa waliyafanya hayo makosa yote, nalichukizwa nao. Kwa hiyo niliwaambia ninyi: Ninyi mtaichukua nchi yao, iwe yenu, mimi nitawapa kuichukua hiyo nchi ichuruzikayo maziwa na asali. Mimi ni Bwana Mungu wenu niliyewatenga na kuwatoa katika makabila mengine. Nanyi mwapambanue nyama wenye kutkata nao wenye uchafu, nao ndege wenye uchafu nao wenye kutakata, msijifanye wenyewe kuwa tapisho kwa ajili ya nyama na ndege, wala kwa ajili ya wadudu wote watambaao katika nchi, niliowatenga kuwa kwenu wenye uchafu. Ndipo, mtakapokuwa watakatifu wangu, kwani mimi Bwana ni mtakatifu, nikawatenga ninyi na kuwatoa katika makabila yote, mwe wangu. Mtu mume au mke akiwa mwenye roho ya kutiisha mizimu au mwenye roho ya kuagua sharti wauawe kwa kupigwa mawe, maana wamekora manza za kuuawa. Bwana akamwambia Mose: Waambie watambikaji, wana wa Haroni, kwamba: Mtambikaji asijipatie uchafu kwa kugusa mfu kwao walio ukoo wake, ila kwao tu walio ndugu zake wa kuzaliwa nao, maana ndio walio kwake karibu: mama yake na baba yake na mwanawe wa kiume na wa kike na mkubwa au mdogo wake, hata umbu lake aliyezaliwa naye akiwa ni mwanamwali bado, asipokuwa bado na mwanamume, basi, hata kwake ataweza kujipatia uchafu. Lakini kwa mwingine aliye wa ukoo wake, ijapo awe mkuu, asijipatie uchafu wa kuupoteza utakatifu wake. Wasijinyoe vichwani kuwa wenye kipara, wala ndevu zao wasizikate pembenipembeni, wala wasijichore nembo miilini mwao. Sharti wawe watakatifu wa Mungu wao, wasilibezeshe Jina la Mungu wao. Kwani ndio wanaozitoa ng'ombe za tambiko za kumteketezea Bwana, zilizo chakula chake Mungu wao, kwa hiyo sharti wawe watakatifu. Mwanamke mgoni wasimchukue wala asiye mwenye macheo, wala mwanamke aliyefukuzwa na mumewe wasimchukue, kwani yeye ni mtakatifu wa Mungu wake. Nawe sharti umwazie kuwa mtakatifu kwa kuwa yeye ndiye anayemtolea Mungu wako chakula chake, kwa hiyo awe mtakatifu kwako, kwani mimi Bwana ninayewatakasa ninyi ni mtakatifu. Binti mtambikaji akianza kuzini humbezesha baba yake, kwa hiyo sharti ateketezwe kwa moto. Naye aliye mtambikaji mkuu miongoni mwa ndugu zake aliyemiminiwa kichwani pake mafuta ya kumpaka, aliyejazwa gao lake, apate kuyavaa yale mavazi yampasayo, asiziache wazi nywele za kichwani pake, wala asizirarue nguo zake, wala asiingie mo mote mwenye mfu ye yote, asijipatie uchafu, wala kwa baba yake wala kwa mama yake. Asitoke Patakatifu, asipapatie Patakatifu pa Mungu wake uchafu, kwani amekwisha kuvikwa kilemba, ndio mafuta ya Mungu wake yaliyompaka. Mimi ni Bwana. Naye mwanamke, atakayemchukua, sharti awe mwanamwali. Asichukue mjane wala aliyefukuzwa na mumewe wala mgoni asiye mwenye macheo, ila achukue mwanamwali tu aliye wa ukoo wao, apate kuwa mkewe. Ni kwamba: asiwatie uchafu walio wa uzao wake kwao walio ukoo wake, kwani mimi Bwana ndiye aliyemtakasa. Bwana akamwambia Mose kwamba: Mwambie Haroni kwamba: Mtu aliye wa vizazi vitakavyozaliwa nao walio wa uzao wako, kama ni mwenye kilema, asije kumtolea Mungu wake chakula chake. Kila mtu mwenye kilema asinikaribie, kama ni kipofu au kiwete au mwenye pua mbaya au mwenye kiungo kilicho kirefu zaidi, au kama ni mtu aliyevunjika mguu au mkono, au kama ni mwenye nundu au mwenye kifua kikuu au mwenye chongo au mwenye upele mbaya au mwenye buba au mwenye mapumbu yaliyovunjika. Kila mwenye kilema aliye wa uzao wake mtambikaji Haroni asije kumtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa; kwa kuwa mwenye kilema asije kumtolea Mungu wake chakula chake. Lakini kula ataweza kula chakula cha Mungu wake kilicho kitakatifu chenyewe nacho kilicho kitakatifu. Asiingie tu hapo mbele ya lile pazia, wala asiijie meza ya kutambikia kwa kuwa mwenye kilema, asipapatie Patakatifu pangu uchafu. Kwani mimi ni Bwana anayepatakasa. Nayo maneno haya Mose akamwambia Haroni na wanawe na watu wote wa Isiraeli. Bwana akamwambia Mose kwamba: Mwambie Haroni nao wanawe, wajiangalie sana kwa ajili ya vipaji vitakatifu vya wana wa Isiraeli wasilibezeshe Jina langu takatifu, maana wanavitoa kuwa vitakatifu vyangu mimi Bwana. Waambie: Hivi vinavipasa vizazi vyenu vitakavyokuwa: mtu ye yote aliye wa uzao wenu wo wote akavifikia karibu vipaji vitakatifu, wana wa Isiraeli wanavyomtolea Bwana kuwa vitakatifu vyake, basi, akivikaribia na kuwa mwenye uchafu, sharti ang'olewe, atoweke usoni pangu; mimi ni Bwana. Mtu ye yote aliye wa uzao wake Haroni akiwa mwenye ukoma au kisonono asile vipaji vitakatifu, mpaka atakapokuwa mwenye kutakata. Atakayegusa mtu aliyejipatia uchafu kwa mfu au aliyetokwa na mbegu alipolala usingizi, au mtu atakayegusa dudu ye yote wa kumpatia uchafu au atakayegusa mtu wa kumpatia uchafu kwa kuwa mwenye uchafu wo wote, basi, atakayegusa cho chote kilicho hivyo ni mwenye uchafu mpaka jioni, kisha asile vitakatifu, asipokuw ameuogesha mwili wake majini. Jua likiisha kuchwa, atakuwa mwenye kutakata; ndipo, atakapoweza kula vitakatifu, kwani ndio chakula chake. Nyama aliyekufa kibudu au aliyeraruliwa na nyama mwingine asile, asijipatie uchafu kwake. Mimi ni Bwana. Na wayaangalie maagizo yangu yawapasayo kuyaangalia, wasijitwike kosa la kuyakosea, wakauawa nalo kwa kuchafua vitakatifu. Mimi ni Bwana anayewatakasa. Lakini mgeni ye yote asile kilicho kitakatifu, wala mtu akaaye mwa mtambikaji wala amfanyiaye kazi ya mshahara asile kilicho kitakatifu. Lakini mtambikaji akinunua mtumishi kwa fedha zake, yeye ataweza kula; nao watumwa watakaozaliwa nyumbani mwake wataweza kula hicho chakula chake. Tena binti mtambikaji akiolewa na mtu mgeni hana ruhusa kula vipaji vitakatifu vya kunyanyuliwa. Lakini binti mtambikaji atakapokuwa mjane au atakapofukuzwa na mumewe hakuzaa watoto, kisha akirudi kukaa nymbani mwa baba yake, kama akiwa alivyokaa katika ujana wake, ataweza kukila chakula cha baba yake; lakini mgeni ye yote asikile. Mtu akila kitakatifu pasipo kukijua, sharti amrudishie mtambikaji hicho kitakatifu na kukiongezea fungu lake la tano. Watambikaji wasivichafue vipaji vitakatifu vya wana wa Isiraeli, wanavyomnyanyulia Bwana, huku ni kwamba, wasiwakoseshe Waisraeli kukora manza za kula wenyewe vipaji vyao vitakatifu. Kwani mimi ni Bwana anayevitakasa. Bwana akamwmbia Mose kwamba: Sema na Haroni na wanawe na wana wote wa Isiraeli na kuwaambia: Mtu ye yote, kama ni wa mlango wa Isiraeli, au kama ni mgeni akaaye kwao Waisiraeli, akitaka kutoa toleo lake, kama ni la kulipa yo yote, aliyoyaapa, au kama ni kwa kupendezwa tu, basi, mtu akitaka kumtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kujipendezesha kwake, sharti iwe dume asiye na kilema, kama ni la ng'ombe au la kondoo au la mbuzi. Kila nyama mwenye kilema msimtoe, kwani hatawapendezesha kwake. Hata mtu akitaka kumtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya shukrani, kama ni ya kuyalipa aliyoyaapa, au kama ni ya kupenda kwa moyo tu, kama anatoa ng'ombe au kama anatoa mbuzi au kondoo, sharti awe pasipo kilema, apate kupendeza, asiwe nyama mwenye kilema cho chote, kama mwenye upofu au mwenye kuvunjika kiungo au mwenye kidonda au mwenye majipu au mwenye kifua kikuu au mwenye upele; nyama aliye hivyo msimtolee Bwana, wala msimteketezee Bwana vipande vyake mezani pa kutambikia. Ng'ombe au kondoo mwenye viungo virefu zaidi au mwenye viungo vifupi zaidi utaweza kumtoa ukipenda mwenyewe kwa moyo, lakini haitafaa kumtoa kuwa wa kuyalipa uliyoyaapa. Nyama mwenye mapumbu yaliyopondwa au yaliyosetwa au yaliyovunjwavunjwa au nyama aliyekatwa mapumbu kabisa msimtolee Bwana. Mtakapofika katika nchi yenu msivifanye. Ijapo mpewe nyama walio hivyo na mtu mgeni, msimtolee Mungu wenu mmoja tu aliye hivyo kuwa chakula chake, kwani nyama hao sio wazima, ni wenye vilema; kwa hiyo hawatawapendezesha. Bwana akamwambia Mose kwamba: Ng'ombe au kondoo au mbuzi akiisha kuzaliwa sharti akae siku saba kwa mama yake. Tangu siku ya nane na baadaye atafaa wa kumtolea Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa. Lakini ng'ombe au kondoo msimchinje siku moja pamoja na mtoto wake. Mkimtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya kumtukuza, sharti mmchinje kwa njia itakayowapendezesha. Sharti aliwe siku iyo hiyo, msisaze hata kidogo mpaka kesho. Mimi ni Bwana. Yaangalieni maagizo yangu, myafanye! Mimi ni Bwana. Msilichafue Jina langu takatifu, nipate kutakaswa katikati yao wana wa Isiraeli. Mimi ni Bwana anayewatakasa ninyi. Niliwatoa ninyi katika nchi ya Misri, niwe Mungu wenu, mimi Bwana. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na wana wa Isiraeli ukiwaambia: Sikukuu za Bwana, mtakazozitangaza kuwa za kukutania Patakatifu, hizo sikukuu zangu ndizo hizi: Kazi sharti zifanywe siku sita, lakini siku ya saba ni siku ya kupumzika kabisa ya kukutania Patakatifu; hapo isifanywe kazi yo yote, maana ndiyo siku ya mapumziko ya kumheshimu Bwana katika makao yenu yote. Hizi ndizo sikukuu za Bwana za kukutania Patakatifu, nanyi sharti mzitangaze, siku zao zilizowekwa zitakapotimia: Katika mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne ya mwezi saa za jioni ni Pasaka ya Bwana. Siku ya kumi na tano ya mwezi uo huo ni sikukuu ya Bwana ya Mikate isiyochachwa; ndipo mle siku saba mikate isiyochachwa. Siku ya kwanza na mkutanie Patakatifu, msifanye kazi yo yote ya utumishi, ila mmtolee Bwana siku saba ng'ombe za tambiko za kuteketezwa. Siku ya saba mkutanie tena Patakatifu, msifanye kazi yo yote ya utumishi. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na wana wa Isiraeli ukiwaambia: Mtakapoingia katika nchi hiyo, nitakayowapa, hapo mtakapoyavuna mavuno yake, mganda wa kwanza wa mavuno yenu sharti mwupeleke kwa mtambikaji. Naye aupitishe motoni huo mganda mbele ya Bwana, uwapendezeshe kwake. Kesho yake siku ya mapumziko ndipo mtambikaji aupitishe motoni. Tena siku hiyo ya kuupitisha mganda wenu motoni sharti mtengeneze mwana kondoo wa mwaka mmoja asiye na kilema kuwa ng'ombe ya tambiko ya Bwana ya kuteketezwa nzima pamoja na vilaji vyake vya tambiko: pishi moja ya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta wa kumteketezea Bwana kuwa mnuko wa kumpendeza, tena kibaba kimoja cha mvinyo kuwa kinywaji chake cha tambiko. Msile mikate ya ngano mpya wala bisi wala chenga za masuke machanga mpaka siku hiyo, mtakapomtolea Mungu wenu vipaji hivyo vya tambiko. Maongozi haya na yawe ya kale na kale kwa vizazi vyenu po pote, mtakapokaa. Kuanzia kesho yake siku ya mapumziko, ni siku ile mlipoupeleka mganda wa kupitishwa motoni, mjihesabie majuma mazima saba, yatimie; siku zao, mtakazozihesabu mpaka kesho yake siku ya mapumziko ya saba ni siku 50; zikitimia, ndipo mmtolee Bwana vilaji vipya vya tambiko. Makaoni mwenu mtoe mikate miwili ya kupitishwa motoni iliyotengenezwa kwa pishi moja ya unga mwembamba, iliyookwa ilipokwisha kuchachuka, ipate kuwa malimbuko ya Bwana. Pamoja na hiyo mikate sharti mpeleke wana kondoo saba wa mwaka mmoja wasio na vilema na ndama mmoja dume na madume mawili ya kondoo, wawe ng'ombe za tambiko za Bwana za kuteketezwa nzima pamoja na vilaji na vinywaji vyao vya tambiko; vikichomwa moto viwe mnuko mzuri wa kumpendeza Bwana. Kisha sharti mtengeneze dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo na wana kondoo wawili wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Kisha mtambikaji awapitishe motoni pamoja na hiyo mikate ya malimbuko kuwa kipaji cha kupitishwa motoni mbele ya Bwana pamoja na hawa wana kondoo wawili; kwa kuwa hawa ni watakatifu wa Bwana, watakuwa mali za watambikaji. Siku hiyo sharti mtangaze, watu wenu wakutanie Patakatifu, msifanye kazi yo yote ya utumishi. Maongozi haya na yawe ya kale na kale kwa vizazi vyenu po pote, mtakapokaa. Mtakapovuna mavuno ya nchi yenu msikate napo pembeni penye mashamba yenu kupavunia napo, wala msiokoteze viokotezo vya mavuno yenu, ila mviache, viokotezwe na wakiwa na wageni. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waambie wana wa Isiraeli kwamba: Katika mwezi wa saba siku ya kwanza ya mwezi iwe kwenu siku ya mapumziko ya ukumbusho wa kupiga baragumu, mtakapokutania Patakatifu. Msifanye kazi yo yote ya utumishi, ila mmtolee Bwana ng'ombe za tambiko. Bwana akamwambia Mose kwamba: Siku ya kumi ya huo mwezi wa saba ni siku ya Mapoza, napo ndipo mkutanie Patakatifu pamoja na kujitesa kwa kufunga na kumtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa. Siku hiyo msifanye kabisa kazi yo yote, kwani ndio siku ya Mapoza ya kuwapatia ninyi upozi mbele ya Bwana Mungu wenu. Kila asiyejitesa mwenyewe kwa kufunga siku hiyohiyo atang'olewa kwao walio ukoo wake. Naye kila atakayefanya kazi yo yote siku hiyohiyo nitamwangamiza kabisa, atoweke katikati yao walio ukoo wake. Kwa hiyo msifanye kazi yo yote. Maongozi haya na yawe ya kale na kale kwa vizazi vyenu po pote, mtakapokaa. Iwe kwenu siku ya mapumziko ya kupumzika kabisa ya kujitesa kwa kufunga. Sharti mpumzike jioni ile siku ya tisa ya mwezi huo toka hapo jioni, ikiwa jioni tena, mpumzike kwa kuishika hiyo siku yenu ya mapumziko. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waambie wana wa Isiraeli: Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya Bwana ya Vibanda siku saba. Siku ya kwanza na mkutanie Patakatifu, msifanye kazi yo yote ya utumishi. Siku saba sharti mmtolee Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa; siku ya nane na mkutanie Patakatifu, mmtolee Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa, ni siku ya mkutano, kwa hiyo msifanye kazi yo yote ya utumishi. Hizi ndizo sikukuu za Bwana, ndipo mtangaze, watu wakutanie Patakatifu kumtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa: za kuteketezwa nzima pamoja na vilaji vya tambiko, tena ng'ombe za tambiko za kuchinjwa pamoja na vinywaji vya tambiko, kila moja siku yake, kama siku inavyopaswa. Lakini tena ziko siku za mapumziko za Bwana na vipaji, mnavyovitoa wenyewe, hata vipaji, mnavyovitoa kwa kuyalipa mliyoyaapa, na vipaji vinginevingine, mnavyomtolea Bwana kwa kupendezwa mioyoni. Siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, mtakapokuwa mmekwisha kuyachuma mapato ya nchi, sharti mle sikukuu ya Bwna siku saba, siku ya kwanza ni ya mapumziko, nayo ya nane ni ya mapumziko. Tena siku ya kwanza na mjipatie matunda mazuri ya miti na makuti mabichi ya mitende na matawi ya miti ya maporini na ya mitoni, mmfurahie Bwana Mungu wenu siku saba. Siku hiyo iliyo sikukuu ya Bwana sharti mwile kila mwaka siku saba. Maongozi haya na yawe ya kale na kale kwa vizazi vyenu, mwile sikukuu hii siku saba. Na mkae vibandani siku saba, wote walio wenyeji kwao Waisiraeli na wakae vibandani. Ni kwa kwamba vizazi vyenu wajue, ya kuwa niliwakalisha vibandani nilipowatoa katika nchi ya Misri. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Mose akawaambia wana wa Isiraeli hizo sikukuu za Bwana. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waagize wana wa Isiraeli, wakupatie mafuta ya chekele yaliyotwangwa vema kuwa safi ya kinara ya kutia siku zote katika taa zake. Hapo nje ya pazia penye Sanduku la Ushahidi katika Hema la Mkutano Haroni azitengeneze hizo taa, ziwake tangu jioni hata asubuhi mbele ya Bwana pasipo kukoma. Maongozi haya na yawe ya kale na kale kwa vizazi vyenu. Penye kile kinara cha dhahabu tupu na azitengeneze taa zake, ziwake mbele ya Bwana siku zote. Tena uchukue unga mwembamba, uuoke kuwa mikate kumi na miwili, kila mikate mmoja uwe wa pishi moja ya unga. Kisha uiweke mistari miwili, kila mstari wenye mikate sita, juu ya meza ya dhahabu tupu mbele ya Bwana. Kisha uweke juu ya kila mstari uvumba ulio safi, uwe moto wa kumpendeza Bwana na kumkumbusha hiyo mikate. Kila siku ya mapumziko sharti aitengeneze tena mbele ya Bwana pasipo kukoma. Hili na liwe agano la kale na kale nao wana wa Isiraeli, wasiache kuitoa. Kisha hiyo mikate itakuwa yao Haroni na wanawe, nao sharti waile mahali patakatifu. Kwa kuwa mitakatifu yenyewe sharti iwe fungu lao litokalo kwenye mioto ya Bwana. Hii na iwe haki yao ya kale na kale. Ikawa, mwana wa mwanamke wa Kiisiraeli mwenye baba wa Kimisri alipotokea katikati ya wana wa Isiraeli, huyu mwana wa mwanamke wa Kiisiraeli akagombana na mtu wa Kiisiraeli makambini. Naye yule mwana wa mwanamke wa Kiisiraeli akalitukana Jina la Bwana pamoja na kuliapiza. Ndipo, walipompeleka kwa Mose, nalo jina la mama yake lilikuwa Selomiti, binti Diburi, wa shina la Dani. Wakamweka kifungoni, wapate kuelezwa, kinywa cha Bwana kitakavyowaambia. Bwana akamwambia Mose kwamba: Huyo mwenye kutukana mtokeze nje ya malago, kisha wote walioyasikia na wambandikie mikono yao kichwani pake, kisha watu wote wa mkutano huu na wamwue kwa kumpiga mawe. Lakini wana wa Isiraeli waambie kwamba: Mtu ye yote atakayemwapiza Mungu wake sharti alipishwe hilo kosa lake. Atakayelitukana Jina la Bwana sharti auawe kabisa, watu wote wa mkutano huu wakimpiga mawe. Kama ni mgeni au kama ni mwenyeji, kwa kulitukana hilo Jina hana budi kuuawa. Mtu akimpiga mwenzake, afe, sharti auawe naye. Lakini akipiga nyama, naye akifa, sharti amlipe, nyama aliye mzima kwa yule aliyekufa. Mtu akimwumiza mwenziwe, apate kilema, naye sharti afanyiziwe yaleyale, aliyoyafanya: kidonda kwa kidonda, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kilema, alichompatia mwenzake, apatiwe naye. Ni hivi: mtu atakayempiga nyama, naye akifa, sharti amlipe; lakini mtu atakayempiga mwenziwe, naye akifa, sharti auawe. Hukumu za kwenu sharti ziwe moja, mwenye kuhukumiwa kama ni mgeni au kama ni mwenyeji. Kwani mimi Bwana ni Mungu wenu. Mose alipokwisha kuwaambia wana wa Isiraeli maneno haya, wakamtokeza yule mwenye kutukana nje ya makambi, wakamwua kwa kumpiga mawe; wana wa Isiraeli wakafanya, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Bwana akamwambia Mose kule mlimani kwa Sinai kwamba: Sema na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Mtakapoingia katika nchi hiyo, nitakayowapa, hiyo nchi nayo sharti ipate kumpumzikia Bwana. Miaka sita upande mbegu mashambani kwako, tena miaka sita uikatie mizabibu yako, upate kuyachuma mazao yao. Lakini mwaka wa saba sharti uiwie nchi yako mwaka wa kupumzika kabisa, nayo ipate kumpumzikia Bwana. Hapo usipande mbegu mashambani kwako, wala usiikatie mizabibu yako. Nayo masazo ya mavuno yako, kama yataota yenyewe, usiyavune, wala zabibu zitakazozaliwa na mizabibu, usiyoitunza, usizichume, kwani mwaka huu sharti uwe kabisa mwaka wa mapumziko ya nchi. Nchi itakayoyazaa katika mwaka wa mapumziko, na myale ninyi na watumishi wako na vijakazi wako na watu wako wa mshahara nao wageni watakaokaa kwako, nao nyama wako wa kufuga na nyama wa porini walioko katika nchi yao; hao wote na wayale mazao yake. Tena uhesabu miaka saba ya mapumziko, ndio miaka saba mara saba, siku za hiyo miaka saba ya mapumziko ziwe kwako miaka 49. Ndipo upige baragumu lenye sauti kuu katika mwezi wa sababu siku ya kumi ya mwezi. Siku ya Mapoza sharti mpige mabaragumu po pote katika nchi yenu yote nzima. Mwaka huo wa 50 sharti mwutakase na kuwatangazia wote wakaao katika nchi yenu, ya kuwa wamekwisha kukombolewa. Mwaka huo uwe wa kupiga shangwe kwenu, mkirudia kila mtu mali zilizokuwa zake, tena mkirudi kila mtu kwa ndugu zake. Kweli mwaka huo wa hamsini sharti uwe kwenu mwaka wa kupiga shangwe, msipande mbegu, wala msiyavune yatakayoota yenyewe, wala msiyachume mazao ya mizabibu, msiyoitunza. Kwani ndio mwaka wa shangwe, nao sharti uwe mtakatifu kwenu, myale tu mashambani yatakayozaliwa. Katika mwaka ulio wa shangwe kila mtu wa kwenu sharti azirudie mali zilizokuwa zake. Kwa hiyo akimwuzia mwenzake kitu au akinunua kitu mkononi mwa mwenzake, msidanganyane wenyewe na wenyewe. Ukinunua shamba kwa mwenzako, sharti mwihesabu miaka iliyopita tangu mwaka wa shangwe, ndipo akuuzie kwa kuipunguza hiyo miaka, aliyolivuna. Miaka itakayosalia ikiwa mingi, mwiongeze bei yake; lakini miaka itakayosalia ikiwa michache, mwipunguze bei yake, kwani yeye hukuuzia mavuno ya miaka tu inayohesabika. msidanganyane wenyewe na wenyewe. Sharti mmwogope Mungu wenu, kwani mimi Bwana ni Mungu wenu. Yafanyeni maongozi yangu na maamuzi yangu mkiyaangalia na kuyafanya! Ndipo, mtakapokaa katika nchi hiyo na kutulia. Nayo nchi hiyo itawapa mazao yake, mle na kushiba, nanyi mtakaa huko na kutulia. Mkiuliza: Tutakula nini katika mwaka wa saba, tusipopanda mbegu, tena tusipoyakusanya mapato yatupasayo? jueni: Katika mwaka wa sita nitawaagizia neema yangu, huo mwaka uwapatie mapato ya miaka mitatu. Mpande tena mbegu katika mwaka wa nane mkila mapato ya kale; mpaka mtakapoingiza mavuno ya mwaka wa tisa, na myale yale ya kale. Nchi isiuzwe kabisa kabisa! Kwani nchi ni yangu mimi, nanyi m wageni tu wanaokaa kwangu. Po pote, mtakapotwaa nchi kuwa yenu, sharti mwache njia ya kuikomboa hiyo nchi. Ndugu yako akiuza kipande cha shamba, alilolitwaa kuwa lake, kwa kukosa mali, tena akija mkombozi wake aliye ndugu yake wa kuzaliwa naye, basi, na akikomboe hicho kipande, ndugu yake alichokiuza. Kama mtu hana mkombozi, lakini akiweza kujipatia kwa mkono wake mali zitoshazo za kukikomboa, na aihesabu hiyo miaka iliyopita tangu hapo, alipokiuza, nazo mali zitakazosalia sharti amrudishie yule mtu aliyemwuzia hicho kipande cha shamba. Hivyo ndivyo, atakavyokirudia, kiwe chake tena. lakini asipoweza kujipatia kwa mkono wake mali zitoshazo, basi, hicho kipande cha shamba, alichokiuza, kitakaa mkononi mwake yule aliyemwuzia, hata mwaka wa shangwe utakapotimia; katika huo mwaka wa shangwe kitatoka mkononi mwake yule, mwenyewe apate kukirudia, kiwe mali yake tena. Mtu akiuza nyumba ya kukaa katika mji wenye boma, sharti apate mwaka mzima wa kuikomboa; hizo na ziwe siku zake za kuikomboa. Lakini isipokombolewa, hata mwaka wote mzima utimie, basi, hiyo nyumba iliyomo mjini mwenye boma itakuwa kabisa kabisa yake aliyeinunua kuwa yake yeye mwenyewe na ya vizazi vyake, haitatoka kwao katika mwaka wa shangwe. Lakini nyumba za vijiji vya huko nje po pote visivyo vyenye maboma na ziwaziwe kuwa sawa na mashamba ya hiyo nchi, ziwezekane kukombolewa, tena katika mwaka wa shangwe zitoke kwake mnunuzi. Namo mijini mwa Walawi nyumba za hiyo miji waliyopewa kuwa fungu lao, zitaweza kukombolewa na Walawi kila mwaka. Kama mtu anakomboa kwao Walawi nyumba au mji, katika mwaka wa shangwe itatoka kwake na kukoma kuwa mali yake, kwani nyumba za miji ya Walawi ni fungu lao walilopewa kuwa lao kabisa katikati ya wana wa Isiraeli. Lakini malisho ya miji yao hayauziki, kwani ni fungu lao kuwa yao kale na kale. Ndugu yako akipatwa na ukosefu wa mali, asiweze tena kushikana mkono na wewe, sharti umpokee kuwa mgeni akaaye kwako na kujitunza kwako. Usimtoze faida ya kukopesha iliyo nyingi, ila umwogope Mungu wako, ndugu yako apate kujitunza kwako. Wala usimkopeshe fedha zako kwa kujitakia faida, wala usimpe chakula chake kwa kujitakia malipo yapitayo kiasi. Mimi Bwana ni Mungu wenu aliyewatoa ninyi katika nchi ya Misri, niwape nchi ya Kanaani, niwe Mungu wenu. Ndugu yako akipatwa na ukosefu wa mali hapo alipo, akajiuza kwako, usimfanyishe kazi za utumwa. Ila awe kwako kama mtu wa mshahara au kama mwingine akaaye kwako. Naye na akutumikie, hata mwaka wa shangwe utimie. Ndipo, atakapopata kutoka kwako, yeye pamoja na watoto wake, arudi kwao walio ndugu zake, tena na alirudie fungu lao lililokuwa lao baba zake. Kwani ndio watumwa wangu mimi, niliowatoa katika nchi ya Misri, hawawezekani kuuzwa kuwa watumwa wenyewe. Nawe usimtawale kwa ukorofi, ila umwogope Mungu wako! Kama unataka kuwa mwenye watumwa wako na vijakazi wako, jinunulie watumwa na vijakazi kwao wamizimu watakaokaa na kuwazunguka ninyi. Hata kwa wana wao watakaokaa kwenu ugenini mtaweza kujinunulia, hata kwao wa uzao wao wataokaa kwenu, wao watakaozaliwa katika nchi yenu, basi, hao wataweza kuwa mali zenu. Hata wana wenu wataokuwa nyuma yenu mtaweza kuwaachilia hao kuwa urithi wao wa mali zitakazokuwa zao kale na kale, nao mwafanyishe kazi za utumwa. Lakini ndugu zenu walio wana wa Isiraeli msitawalane wenyewe na wenyewe kwa ukorofi. Mgeni au mwingine atakayekaa kwako akijipatia mali kwa kazi za mkono wake, naye ndugu yako anapatwa na ukosefu wa mali hapo alipo huyo, akajiuza kwake huyo mgeni au kwa mwingine atakayekaa kwako au kwa mwingine aliye wa ukoo mgeni, sharti awe na njia ya kukombolewa akiisha kujiuza; kila mmoja wao walio ndugu zake ataweza kumkomboa, au baba yake mkubwa au mdogo, au mwanawe ataweza kumkomboa, au mmoja wao waliozaliwa naye katika mlango wake ataweza kumkomboa au mwenyewe ataweza kujikomboa akijipatia mali za kutosha kwa kazi za mkono wake. Ndipo yeye pamoja naye aliyemnunua na waihesabu miaka tangu hapo, alipojiuza mpaka hapo, mwaka wa shangwe utakapotimia, kisha fedha za kumnunua na zigawanywe sawasawa kwa hesabu ya hiyo miaka kuwa kama mshahara wa miaka ya mtu wa kazi. Kama miaka iko mingi bado, basi, katika hizo fedha, alizozipata alipojiuza, na arudishe hizo ziipasazo miaka iliyosalia kuwa makombozi yake. Lakini kama miaka iko michache bado, mpaka mwaka wa shangwe utakapotimia, basi, na azirudishe hizo tu ziipasazo hiyo miaka yake michache kuwa makombozi yake. Kwake Bwana wake na awe kama mtu wa kazi za mshahara mwaka kwa mwaka, naye yule asimtawale kwa ukorofi machoni pako. Asipokombolewa kwa njia hii, atatoka utumwani katika mwaka wa shangwe, yeye pamoja na watoto wake. Kwani wana wa Isiraeli ni watumwa wangu mimi; ndio watumwa wangu, niliowatoa katika nchi ya Misri. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Msijitengenezee vinyago vilivyo vya bure! Wala msijisimamishie mifano ya Mungu iliyochongwa kwa miti wala ya nguzo zilizoyeyushwa kwa shaba, wala msijipatie katika nchi yenu mawe yenye machorochoro ya kuyaangukia. Kwani mimi Bwana ni Mungu wenu. Siku zangu za mapumziko sharti mziangalie, napo Patakatifu pangu sharti mpache. Mimi ni Bwana. Kama mtayafuata maongozi yangu, myaangalie maagizo yangu na kuyafanya, nitawapa mvua zenu, siku zao zitakapotimia, nchi ipate kuyatoa mazao yake, nayo miti ya mashambani ipate kuyatoa matunda yao. Ndipo, siku za kupura zitakapopokelewa na siku za kuchuma zabibu, nazo siku za hayo machumo zitapokelewa na siku za kupanda, nanyi mtakula chakula chenu na kushiba, mkae katika nchi yenu na kutulia. Maana hiyo nchi nitaipatia utengemano, mpate kulala pasipo kustushwa, nao nyama wabaya nitawatoa katika hiyo nchi, wala upanga hautapita katika nchi yenu. Mtakapowakimbiza adui zenu, wataangushwa kwa panga mbele yenu. Watu watano wa kwenu watakimbiza mia, nao mia wa kwenu watakimbiza maelfu kumi; ndivyo, adui zenu watakavyoangushwa kwa panga mbele yenu. Nami nitwageukia, niwape kuzaa, mpate kuwa wengi, kwani nitalitimiza Agano langu, nililolisimika nanyi. Mtakula ngano za kale zilizowekwa kale, tena hizo za kale mtaziondoa tu, mpate pa kuziwekea mpya. Nalo Kao langu nitaliweka katikati yenu, kwa kuwa Roho yangu haitawachukia. Nitatembea katikati yenu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa ukoo wangu. Mimi Bwana ni Mungu wenu aliyewatoa katika nchi ya Misri, msiwe watumwa wao, nayo miti ya makongwa yenu nikaivunja, nikawapa kujiendea na kujinyosha. Lakini msiponisikia, msiyafanye maagizo haya yote, myakatae maongozi yangu, roho zenu zikichukiwa na maamuzi yangu, msiyafanye maagizo yangu yote na kulivunja Agano langu, ndipo, mimi nitakapowafanyizia haya: nitatuma kwenu mastusho na kifua kikuu na homa; magonjwa haya yatawapofusha macho yenu na kuzizimiza roho zenu. Mtakapopanda mbegu zenu, itakuwa ya bure, kwani adui zenu watazila. Nao uso wangu nitaugeuza, uwapingie, mpigwe mbele ya adui zenu, nao wachukivu wenu wawatwale; nanyi mtajikimbilia pasipo kuona aliyewakimbiza. Ijapo msinisikie napo hapo, nitaendelea kuwapatiliza mara saba kwa ajili ya ukosaji wenu, niyavunje majivuno yenu yaliyo na nguvu nikizifanya mbingu za kwenu kuwa kama chuma nayo nchi yenu kuwa kama shaba. Ndipo, kazi zenu zitakapokuwa za kusumbuka bure tu, kwani nchi yenu haitatoa mazao yake, wala miti ya hiyo nchi haitazaa matunda yao. Ijapo hapo napo mwendelee kupingana na mimi na kukataa kusikia, nitaendelea kuwapatia mapigo yaliyo makali mara saba kwa ajili ya ukosaji wenu. Nitatuma kwenu nyama wa porini, wawaue watoto wenu, wawatoweshe nao nyama wenu wa kufuga, nanyi wenyewe watawapunguza, mwe wachache, nazo njia za kwenu ziwe pasipo watu. Ijapo hapo napo msionyeke, mkaendelea kupingana na mimi, basi, mimi nami nitaendelea kupingana nanyi mimi mwenyewe nikiwapiga tena mapigo yaliyo makali mara saba kwa ajili ya ukosaji wenu: nitapeleka kwenu upanga utakaowalipiza kisasi kwa kulivunja Agano; tena mtakapokusanyika mijini mwenu nitatuma kwenu ugonjwa uuao upesi, kisha mtatiwa mikononi mwa adui zenu. Kisha nitawanyang'anya nacho chakula kilichowaegemeza, wanawake kumi wawaokee mikate katika jiko moja, kisha watawarudishia mikate yenu na kuwapimia kwa mizani, mle pasipo kushiba. Ijapo hapo napo msinisikie, mkaendelea kupingana na mimi, nami nitaendelea kupingana nanyi kwa ukali nikiwachapua machapuo yaliyo makali zaidi mara saba kwa ajili ya ukosaji wenu, mzile nyama za miili yao wana wenu wa kiume nazo nyama za wana wenu wa kike. Napo penu pa kutambikia vilimani nitapabomoa, nayo mifano yenu ya jua nitaitowesha, nayo mizoga yenu nitaitupa juu ya vipande vya magogo yenu ya kutambikia, kwani Roho yangu itakuwa imechukizwa nanyi. Hata miji yenu nitaigeuza kuwa mabomoko tu, nazo nyumba zenu takatifu nitaziacha, ziwe peke yao tu, nisiusikie tena mnuko wenu ulionipendeza. Hata nchi yenu nitaiacha, iwe peke yake tu, adui zenu wapate kuistukia watakapokaa huko. Nanyi wenyewe nitawatawanya kwao wamizimu, kisha na mimi nitauchomoa upanga nyuma yenu; ndipo, nchi yenu itakapokuwa pori tupu, nayo miji yenu itakuwa mabomoko tu. Ndipo, nchi yenu itakapopendezwa na kuipata miaka yake ya mapumziko siku zile zote, itakapokuwa pori tupu, ninyi mkikaa katika nchi ya adui zenu. Hapo ndipo, hiyo nchi itakapopumzika kweli na kuilipa miaka yake ya mapumziko. Siku hizo zote za kuwa pori tupu itapata kupumzika, kwa kuwa haikupumzika, ninyi mlipokaa huko na kuinyima miaka ya mapumziko. Nao watakaosalia kwenu nitawalegeza mioyo yao, wakikaa katika nchi ya adui zao, shindo la jani kavu linalopeperushwa na upepo liwakimbize, wakimbie, kama watu wanavyokimbizwa na upanga, waanguke, pasipo kuona aliyewakimbiza. Wataangukiana wenyewe kwa wenyewe, kama watu wanavyoangukiana kwa kukimbia upanga, lakini hatakuwako mwenye kuwakimbiza; nanyi hamtaweza kuwainukia adui zenu. Kule kwa wamizimu ndiko, mtakakoangamia, nayo nchi ya adui zenu ndiyo itakayowala. Nao watakaosalia watazimia na kuyeyuka katika nchi ya adui zenu kwa ajili ya manza zao, walizozikora, hata kwa ajili ya manza, baba zao walizozikora, watayeyuka na kuzimia pamoja nao. Ndipo, watakapoungama, ya kuwa walikora manza, baba zao walizozikora nao, walipoyavunja maagano yangu kwa kuendelea kupingana na mimi. Kwa hiyo mimi nami naliendelea kupingana nao na kuwapeleka katika nchi ya adui zao; lakini hapo, mioyo yao iliyokuwa haikutahiriwa itakapojinyenyekeza kuitikia, ya kuwa walikora manza, ndipo, nami nitakapolikumbuka agano, nililolifanya na Yakobo, nalo agano, nililolifanya na Isaka, nalo agano, nililolifanya na Aburahamu, nayo nchi hiyo nitaikumbuka. Lakini kwanza sharti nchi itokwe nao, ipate kuifurahia miaka yake ya mapumziko ikiwa pori tupu kwa kuachwa nao; nao kwanza sharti waitikie, ya kuwa walikora manza walipoyatupa maamuzi yangu, roho zao zikayachukia maongozi yangu. Lakini hapo napo, watakapokuwa katika nchi ya adui zao, mimi sitawatupa, wala sitawachukia, niwamalize kabisa na kulivunja Agano langu, nililolifanya nao, kwani mimi Bwana ni Mungu wao. Ila kwa kuwatakia wokovu nitalikumbuka Agano, nililolifanya na baba zao wa kwanza nilipowatoa katika nchi ya Misri machoni pa wamizimu, niwe Mungu wao mimi Bwana. Haya ndiyo maongozi na maamuzi na maonyo, Bwana aliyoyatoa kinywani mwa Mose mlimani kwa Sinai kuwa katikati yake yeye nao wana wa Isiraeli. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema nao wana wa Isiraeli na kuwaambia: mtu akitaka kuyalipa, aliyoyaapa ya kujitoa kuwa wake Bwana, sharti wewe uyapime makombozi ya mtu. Nacho kipimo chako ni hiki: mtu mume aliye wa miaka ishirini mpaka sitini makombozi yake, utakayompimia, ni fedha hamsini, zikipimwa na mizani ya Patakatifu. Kama ni mwanamke, makombozi yake utakayompimia, ni fedha thelathini. Akiwa na miaka mitano mpaka ishirini, makombozi yake, utakayompimia, ni fedha ishirini, kama ni mtu mume; kama ni mwanamke, ni fedha kumi tu. Akiwa wa mwezi mmoja mpaka miaka mitano, makombozi yake, utakayompimia, ni fedha tano, kama ni mtu mume; kama ni mwanamke, utampimia makombozi ya fedha tatu tu. Akiwa wa miaka sitini na zaidi, kama ni mtu mume, makombozi yake, utakayompimia, ni fedha kumi na tano; kama ni mwanamke, fedha zake ni kumi. Lakini kama ni mkosefu wa mali, asiweze kuyalipa hayo makombozi, uliyompimia, na wamsimamishe mbele ya mtambikaji, naye mtambikaji na ampimie makombozi yake akiyalinganisha na mali, yule mwenye kuapa anazoweza kuzipata kwa mkono wake; hicho kiwe kipimo chake mtambikaji cha kumpimia hayo makombozi. Kama ni nyama, watu wanayemtolea Bwana kuwa toleo la tambiko, kila mmoja, atakayemtoa katika nyama hao, atakuwa mtakatifu, wasimbadilishe wala wasilete mwingine pia, kama mwema kwa mbaya au mbaya kwa mwema. Kama mtu anabadilisha nyama kwa nyama, wote wawili watakuwa watakatifu, yule wa kwanza na yule, aliyemleta wa kubadili. Kama nyama ni mwenye uchafu, wsiweze kumtolea Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko, na wamsimamishe huyo nyama mbele ya mtambikaji. Naye mtambikaji na ayapime makombozi yake kwa kumpambanua kuwa mwema au mbaya, nayo makombozi yake, mtambikaji atakayoyapima kuwa sawa, basi, yatakuwa yaleyale. Naye kama anataka kumkomboa kweli, ataongeza fungu la tano la hayo makombozi, uliyoyapima. Mtu akiitakasa nyumba yake kuwa kipaji kitakatifu cha Bwana, mtambikaji na ayapime makombozi yake kwa kuipambanua kuwa njema au mbaya; nayo makombozi, mtambikaji atakayoyapima, yatakuwa yaleyale. Kama mwenye kuitakasa anataka kuikomboa na aongeze fungu la tano la fedha, ulizozipima kuwa makombozi yake, kisha itakuwa yake tena. Mtu akitakasa kipande cha shamba lililo fungu lake kuwa mali ya Bwana, utayapima makombozi yake kwa kipimo cha mbegu zinazoenea hapo: kama hicho kipande cha shamba kinataka mbegu za mawele frasila kumi makombozi yake ni fedha hamsini. Kama yule mtu anakitakasa kile kipande cha shamba lake kuanzia katika mwaka wa shangwe, makombozi yake ni yaleyale, uliyoyapima. Kama anakitakasa baada ya mwaka wa shangwe, mtambikaji na amhesabie fedha kwa hesabu ya miaka itakayosalia mpaka mwaka wa shangwe utimie; vivi hivi fedha za makombozi, alizozipima, zitapunguzwa. Kama mwenye kulitakasa shamba lake anataka kulikomboa, sharti aongeze fungu la tano la fedha za makombozi, uliyoyapima, kisha litakuwa lake tena. Lakini kama halikomboi hilo shamba, akaliuza kwa mtu mwingine, haliwezekani kukombolewa tena. Kwani hapo, litakapotoka katika mwaka wa shangwe kwake aliyelinunua, litakuwa mali ya Bwana kama shamba lililotiwa mwiko wa kuwa mali ya mtu; nalo litakuwa fungu lake mtambikaji. Mtu akitoa shamba, alilolinunua, lisilo shamba la fungu lake mwenyewe, akilitakasa kuwa lake Bwana, mtambikaji na amtolee jumla ya fedha, ulizozipima kuwa makombozi yake, mpaka mwaka wa shangwe utakapotimia; nazo hizo, ulizozipima, sharti yule azitoe siku hiyo kuwa mali za Bwana. Katika mwaka wa shangwe shamba hilo litarudi kwake yeye, ambaye alilinunua kwake, maana ni fungu lake la nchi lililo lake mwenyewe. Nayo makombozi yote, utakayoyapima, sharti uyapime kwa fedha zilizopimwa kwa mizani ya Patakatifu, fedha moja iwe ya thumuni nane. Wana wa kwanza wa nyama wa kufuga mtu asiwatakase kuwa wake Bwana, kwani ndio wake Bwana kwa kuzaliwa wa kwanza, kama ni ng'ombe, au kama ni mbuzi au kondoo, ni wake Bwana. Kama ni mwana wa nyama mwenye uchafu, anaweza kumkomboa kwa kulipa makombozi, uliyoyapima, na kuongeza fungu lao la tano; lakini asipomkomboa atauzwa kwa hayo makombozi, uliyoyapima. Yo yote, mtu atakayomtolea Bwana kuwa yake kwa kuyatia mwiko wa kutunzwa na mtu, akiyatoa katika yo yote yaliyo yake yeye, kama ni mtu au nyama wa kufuga au shamba lililo la fungu lake mwenyewe, hayawezekani wala kuuzwa wala kukombolewa, maana yote pia yaliyotiwa mwiko wa kutunzwa na mtu ni matakatifu yenyewe, ni yake Bwana. Mtu ye yote aliyetiwa huo mwiko wa kutunzwa na mtu hawezekani kukombolewa, hana budi kuuawa kabisa. Kila fungu la kumi la nchi, kama ni la mbegu za nchi au kama ni la matunda ya nchi, ni lake Bwana, ni mali takatifu za Bwana. Kama mtu anataka kulikomboa fungu lake la kumi, sharti aongeze fungu la tano la fedha zake. Hata kila fungu la kumi la ng'ombe na la mbuzi na la kondoo, yaani kila atakayepita chini ya fimbo, ni fungu la kumi lililo mali takatifu za Bwana. Hapo watu wasitazame sana, kama ni mwema au kama ni mbaya, wala wasimbadilishe. Kam mtu anambadilisha, yule wa kwanza pamoja na badili yake watakuwa wote wawili mali takatifu za Bwana, wasiwezekane kukombolewa. Haya ndiyo maagizo, Bwana aliyomwagiza Mose mlimani kwa Sinai ya kuwaambia wana wa Isiraeli. Siku ya kwanza ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya kutoka kwao katika nchi ya Misri Bwana akamwambia Mose katika nyika ya Sinai Hemani mwa Mkutano kwamba: Toeni jumla yao wote walio mkutano wa wana wa Isiraeli kwa ndugu zao na kwa milango ya baba zao, mkiyahesabu majina ya wana waume wote kichwa kwa kichwa. Kuanzia kwao wenye miaka ishirini na zaidi wewe na Haroni mwakague wote pia wanaoweza kwenda vitani kwao Waisiraeli, kikosi kwa kikosi. Tena mchukue kuwa nanyi kwa kila shina moja mtu mmoja aliye kichwa chao walio wa mlango wa baba yake. Nayo haya ndiyo majina yao, ninaowataka, wasimame pamoja nanyi: wa Rubeni Elisuri, mwana wa Sedeuri; wa Simeoni Selumieli, mwana wa Surisadai; wa Yuda Nasoni, mwana wa Aminadabu; wa Isakari Netaneli, mwana wa Suari; wa Zebuluni Eliabu, mwana wa Heloni; wa wana wa Yosefu: wa Efuraimu Elisama, mwana wa Amihudi, wa Manase Gamulieli, mwana wa Pedasuri; wa Benyamini Abidani, mwana wa Gideoni; wa Dani Ahiezeri, mwana wa Amisadai; wa Aseri Pagieli, mwana wa Okrani; wa Gadi Eliasafu, mwana wa Deueli; wa Nafutali Ahira, mwana wa Enani. Hawa ndio wateule wa mkutano walio wakuu wa mashina ya baba zao, nao ndio waliokuwa vichwa vya maelfu ya Waisiraeli. Mose na Haroni wakawachukua watu hawa waliotajwa majina yao, wakaukusanya mkutano wote siku ya kwanza ya mwezi wa pili; ndipo, walipoandikwa katika vitabu vya vizazi kwa ndugu zao na kwa milango ya baba zao; yakahesabiwa kichwa kwa kichwa majina yao waliokuwa wenye miaka ishirini na zaidi; kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, alivyowakagua nyikani kwa Sinai. Wana wa Rubeni, mwanawe wa kwanza wa Isiraeli, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina kichwa kwa kichwa, waume wote wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Rubeni walikuwa watu 46500. Wana wa Simeoni, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, walipokaguliwa na kuhesabiwa majina kichwa kwa kichwa, waume wote wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Simeoni walikuwa watu 59300. Wana wa Gadi, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Gadi walikuwa watu 45650. Wana wa Yuda, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwanda vitani, jumla yao wa shina la Yuda walikuwa watu 74600. Wana wa Isakari, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Isakari walikuwa watu 54400. Wana wa Zebuluni, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Zebuluni walikuwa watu 57400. Wanawe Yosefu wana wa Efuraimu, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Efuraimu walikuwa watu 40500. Wana wa manase, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Manase walikuwa watu 32200. Wana wa Benyamini, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Benyamini walikuwa watu 35400. Wana wa Dani, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Dani walikuwa watu 62700. Wana wa Aseri, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Aseri walikuwa watu 41500. Wana wa Nafutali, vizazi vyao vya udugu wao na vya milango ya baba zao, yalipohesabiwa majina yao wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani, jumla yao wa shina la Nafutali walikuwa watu 53400. Hizi ndizo jumla zao, nao waliowakagua ni Mose na Haroni na wale wakuu kumi na wawili wa Waisiraeli waliokuwa kila mmoja wa milango ya baba zao. Nao wana wa Isiraeli wote wa milango ya baba zao waliokaguliwa kuwa wenye miaka ishirini na zaidi, wao wote walioweza kwenda vitani kwao Waisiraeli, jumla yao yote walikuwa watu 603550. Lakini Walawi hawakuhesabiwa katikati yao kwa hivyo, shina la baba zao lilivyokuwa. Bwana akamwambia Mose kwamba: Wao wa shina la Lawi usiwakague, wala jumla yao usiitie katika hiyo ya wana wa Isiraeli. Ila utawaweka Walawi kuliangalia Kao l Ushahidi na vyombo vyake vyote nayo yote yaliyomo. Wao ndio watakaolichukua kao na vyombo vyake vyote, nao ndio watakaolitumikia, nao wakipiga makambi yao, hayo na yalizunguke. Kao litakapoondoka, wao Walawi ndio watakaolishusha chini; tena Kao litakapofika makambini, Walawi ndio watakaolisimamisha; lakini mgeni atakayelikaribia hana budi kuuawa. Wana wa Isiraeli watakapopiga makambi, kila mtu na apige hema katika kambi lake penye bendera ya kikosi cha kwao. Lakini Walawi na wapige makambi kulizunguka Kao la Ushahidi, makali yangu yasiwajie wao wa mkutano wa wana wa Isiraeli; kwa hiyo Walawi na wangoje zamu ya kuliangalia Kao la Ushahidi. Wana wa Isiraeli wakayafanya yote; kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, walivyofanya kuwa sawasawa. Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba: Wana wa Isiraeli na wapige makambi yao kila mtu penye bendera yake, vielekezo vya mlango wa baba zao vilipo; nayo makambi, watakayoyapiga, sharti yalielekee Hema la Mkutano na kulizunguka. Watakaopiga makambi upande wa mashariki wa maawioni kwa jua ndio hawa: bendera ya makambi ya vikosi vyake Yuda iwe huko kwa mkuu wa wana wa Yuda. Nasoni, mwana wa Aminadabu; vikosi vyake jumla yao ni watu 74600. Watakaopiga makambi kando yake ndio wao wa shina la Isakari, naye mkuu wa wana wa Isakari ni Netaneli, mwana wa Suari. Vikosi vyake jumla yao ni watu 54400. Tena wao wa shina la Zebuluni, naye mkuu wa wana wa Zebuluni ni Eliabu, mwana wa Heloni. Vikosi vyake jumla yao ni watu 57400. Jumla yao wote watakaokuwa makambini kwa Yuda ni watu 186400 kwa vikosi vyao, nao ndio wa kwanza watakaoondoka. Upande wa kusini itakuwako bendera ya makambi ya vikosi vya Rubeni, naye mkuu wa wana wa Rubeni ni Elisuri, mwana wa Sedeuri. Vikosi vyake jumla yao ni watu 46500. Watakaopiga makambi kando yake ndio wao wa shina la Simeoni, naye mkuu wao wana wa Simeoni ni Selumieli, mwana wa Surisadai. Vikosi vyake jumla yao ni watu 59300. Tena wao wa shina la Gadi, naye mkuu wa wana wa Gadi ni Eliasafu, mwana wa Reueli. Vikosi vyake jumla yao ni watu 45650. Jumla yao wote watakaokuwa makambini kwa Rubeni ni watu 151450 kwa vikosi vyao, nao ndio wa pili watakaoondoka. Kisha Hema la Mkutano na liondoke pamoja nao wakaao makambini kwa Walawi, liwe katikati ya makambi; kama walivyopanga makambini ndivyo waondoke kwenda kusafiri, kila mtu mahali pake penye bendera ya kwao. Upande wa baharini itakuwako bendera ya makambi ya vikosi vya Efuraimu, naye mkuu wa wana wa Efuraimu ni Elisama, mwana wa Amihudi. Vikosi vyake jumla yao ni watu 40500. Kando yake watakuwako wao wa shina la Manase, naye mkuu wa wana wa Manase ni Gamulieli, mwana wa Pedasuri. Vikosi vyake jumla yao ni watu 32200. Tena wao wa shina la Benyamini, naye mkuu wa wana wa Benyamini ni Abidani, mwana wa Gideoni. Vikosi vyake jumla yao ni watu 35400. Jumla yao wote watakaokuwa makambini kwa Efuraimu ni watu 108100 kwa vikosi vyao, nao ndio wa tatu watakaoondoka. Upande wa kaskazini itakuwako bendera ya makambi ya vikosi vya Dani, naye mkuu wa wana wa Dani ni Ahiezeri, mwana wa Amisadai. Vikosi vyake jumla yao ni watu 62700. Watakaopiga makambi yao kando yake ni wao wa shina la Aseri, naye mkuu wa wana wa Aseri ni Pagieli, mwana wa Okrani. Vikosi vyake ni watu 41500. Tena wao wa shina la Nafutali, naye mkuu wa wana wa Nafutali ni Ahira, mwana wa Enani. Vikosi vyake jumala yao ni watu 53400. Jumla yao wote watakaokuwa makambini kwa Dani ni watu 157600, nao ndio wa mwisho watakaoondoka wakizifuata bendera zao. Hii ndiyo jumla yao wana wa Isiraeli wa milango ya baba zao. Wote waliohesabiwa makambini kwa vikosi vyao jumla yao walikuwa watu 603550. Lakini Walawi hawakuhesabiwa kwao wana wa Isiraeli, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Wana wa Isiraeli wakayafanya yote; kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, walivyoyapiga makambi yao penye bendera zao, tena ndivyo, walivyoondoka kwenda kusafiri kila mtu na ndugu zake penye milango ya baba zao. Hivi ndivyo vizazi vya Haroni na vya Mose vya siku zile, Bwana aliposema na Mose mlimani kwa Sinai. Haya ndiyo majina ya wanawe Haroni: wa kwanza ni Nadabu, tena Abihu na Elazari na Itamari. Haya ndiyo majina ya wanawe Haroni waliopakwa mafuta kuwa watambikaji na kujazwa magao yao, wapate kufanya kazi ya utambikaji. Lakini Nadabu na Abihu walikufa mbele ya Bwana walipomtolea Bwana moto mgeni wa mavukizo nyikani kwa Sinai, nao hawakuwa na wana; kwa hiyo Elazari na Itamari walifanya kazi ya utambikaji na kuangaliwa na baba yao Haroni. Bwana akamwambia Mose kwamba: Wafikishe hawa wana wa shina la Lawi, uwasimamishe mbele ya mtambikaji Haroni, wamtumikie. Tena na waziangalie hizo kazi zinazompasa yeye kuziangalia, nazo kazi zinazoupasa mkutano wote kuziangalia mbele ya hema la Mkutano na kuutumikia utumishi wa Kaoni. Na waviangalie vyombo vyote vya Hema la Mkutano na kuziangalia kazi zinazowapasa wana wa Isiraeli kuziangalia na kuutumikia utumishi wa kaoni. Hawa Walawi umpe Haroni na wanawe, wawe vipaji vyao walivyopewa na wana wa Isiraeli. Nao akina Haroni na wanawe uwaweke kuuangalia utambikaji wao. Lakini mgeni atakayejitia humo hana budi kuuawa. Bwana akasema na Mose kwamba: Tazama, mimi nimewachagua Walawi na kuwatoa katikati ya wana wa Isiraeli kuwa makombozi ya wana watakaozaliwa wa kwanza na mama zao kwa wana wa Isiraeli, kwa hiyo Walawi watakuwa wangu. Kwani wana wa kwanza wote ni wangu, kwani siku hiyo, nilipompiga kila mwana wa kwanza katika nchi ya Misri, nilijitakasia kila mwana wa kwanza kwa Waisiraeli, kama ni wa mtu au kama ni wa nyama wa kufuga, wawe wangu mimi Bwana. Bwana akamwambia Mose nyikani kwa Sinai kwamba: Wakague wana wa Lawi milango ya baba zao mlango kwa mlango na udugu kwa udugu ukiwahesabu waume wote walio wenye mwezi mmoja na zaidi. Kisha Mose akawakagua kwa hiyo amri ya bwana, kama alivyoagizwa. Nao wana wa lawi walikuwa hawa kwa majina yao: Gersoni na Kehati na Merari. Nayo haya ndiyo majina ya wanawe Gersoni wenye udugu wao: Libuni na Simei. Nao wanawe Kehati wenye udugu wao ni Amuramu na Isihari, Heburoni na Uzieli. Nao wanawe Merari wenye udugu wao ni Mahali na Musi. Hawa ndio ndugu za Lawi za milango ya baba zao. Wa Gersoni walikuwa wao wa udugu wa Libuni nao wa udugu wa Simei; hawa ndio ndugu zao wa Gersoni. Walipohesabiwa waume wote wenye mwezi mmoja na zaidi jumla yao walikuwa watu 7500. Hawa ndugu zao wa Gersoni wakaambiwa, wapige makambi nyuma ya Kao upande wa baharini. Naye mkuu wao wa mlango wa baba yao Gersoni awe Eliasafu, mwana wa Laeli. Nazo kazi zao wana wa Gersoni za kuziangalia Hemani mwa Mkutano ziwe kuliangalia Kao lenyewe na Hema na chandalua chake na lile guo kubwa la pazia lililoko pa kuliingilia Hema la Mkutano, nazo nguo za uani na lile guo kubwa la pazia lililoko pa kuuingilia ua, unaolizunguka Kao na meza ya kutambikia, tena kamba zake nayo yote yanyoupasa utumishi huu. Wa Kehati walikuwa wao wa udugu wa Amuramu nao wa udugu wa Isihari nao wa udugu wa Heburoni nao wa udugu wa Uzieli. Hawa ndio ndugu zao wa Kehati. Walipohesabiwa waume wote wenye mwezi mmoja na zaidi jumla yao walikuwa watu 8600 wa kuziangalia kazi za kupaangalia Patakatifu. Hawa ndugu zao wa Kehati wakaambiwa, wapige makambi upande wa kusini wa Kao. Naye mkuu wao wa mlango wa baba yao Kehati awe Elisafani, mwana wa Uzieli. Nazo kazi zake ziwe kuliangalia Sanduku na meza ya mikate na kinara na meza ya kuvukizia nayo ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, navyo vyombo vya Patakatifu, watakavyovitumia, na pazia la Hemani, tena wafanye kazi zote za utumishi uwapasao. Naye mkuu wa wakuu wa Walawi alikuwa Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, awakague wote wanaoangalia kazi za Patakatifu. Wa Merari walikuwa wao wa udugu wa Mahali nao wa udugu wa Musi. Hawa ndio ndugu zao wa Merari. Walipohesabiwa waume wote wenye mwezi mmoja na zaidi jumla yao walikuwa watu 6200. Nao wakaambiwa, mkuu wao wa mlango wa baba yao Merari awe Surieli, mwana wa Abihaili, nao wapige makambi upande wa kaskazini wa Kao. Nazo kazi zao wana wa Merari za kuangalia walizopewa ziwe hizo za mbao za Kao na misunguo yao na nguzo zao na miguu yao na vyombo vyao vyote, wafanye kazi zote za utumishi ziwapasazo, tena kazi za kuziangalia nguzo zilizouzunguka ua na miguu yao na mambo zao na kamba zao. Nao waliopiga makambi mbele ya Kao upande wa mashariki, ndio mbele ya Hema la Mkutano upande wa maawioni kwa jua walikuwa Mose na Haroni na wanawe waliongoja zamu za kupaangalia Patakatifu mahali pao wana wa Isiraeli. Lakini mgeni aliyejitia katika kazi hizi hakuwa na budi kuuawa. Jumla yao Walawi wote, Mose na Haroni waliowakagua kwa amri ya Bwana, waume wote wenye mwezi mmoja na zaidi wa udugu wao walikuwa watu 22000. Bwana akamwambia Mose: Wakague waume wote wa wana wa Isiraeli wenye mwezi mmoja na zaidi walio wana wa kwanza, ufanye hesabu ya majina yao. Uwachukue Walawi kuwa wangu mimi Bwana, wakiwakomboa wana wote wa kwanza kwa wana wa Isiraeli, nao nyama wa kufuga wa Walawi na wawakomboe wana wa kwanza wa nyama wa kufuga wa wana wa Isiraeli. Ndipo, Mose alipowakagua wana wote wa kwanza wa Waisiraeli, kama Bwana alivyomwagiza. Nao waume wote waliokuwa wana wa kwanza wenye mwezi mmoja na zaidi walipohesabiwa majina, jumla yao walikuwa watu 22273. Bwana akamwambia Mose kwamba: Wachukue Walawi kuwa makombozi ya wana wote wa kwanza kwa wana wa Isiraeli, nao nyama wa kufuga wa Walawi kuwa makombozi ya nyama wao, Walawi wawe wangu mimi Bwana. Nayo makombozi yao wale 273 waliozidi kwa wana wa kwanza wa wana wa Isiraeli kuwa wengi kuliko Walawi, uwatoze kila mmoja fedha (sekeli) tano tano kichwa kwa kichwa, nazo hizi fedha, utakazowatoza, ziwe fedha zinazotumika Patakatifu, kila fedha moja iwe ya gera ishirini, ndio thumuni nane. Hizi fedha mpe Haroni na wanawe kwa kuwa makombozi yao wale waliozidi kuwa wengi. Ndipo, Mose alipowatoza fedha za makombozi wale waliozidi kuwa wengi kuliko wale waliokombolewa na Walawi. Nazo hizi fedha, alizozitoza za kuwakomboa wana wa kwanza wa wana wa Isiraeli, zikawa 1365, zikipimwa kwa fedha za Patakatifu. Kisha Mose akampa Haroni na wanawe hizo fedha kwa ile amri ya Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba: Fanyeni hesabu ya wana wa Kehati na kuwatoa kwao wana wa Lawi walio wa udugu wao wa milango ya baba zao. Wao wa miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini ndio wanaofaa wote kuuingia utumishi huo, wafanye kazi za humo Hemani mwa Mkutano. Nazo kazi za utumishi za wana wa Kehati za humo Hemani mwa Mkutano ziwe za Patakatifu Penyewe. Makambi yatakapovunjwa, Haroni na wanawe na waingie Hemani, walishushe lile guo kubwa la pazia, wafunike nalo Sanduku la Ushahidi. Kisha waweke juu yake blanketi la ngozi za pomboo, juu yake tena watandaze nguo nyeusi iliyo ya kifalme yote nzima, kisha na walitie mipiko yake. Hata meza yenye mikate ya kuwa usoni pa Bwana na waifunike kwa nguo nyeusi ya kifalme na kuweka juu yake vyano na vijiko na vikombe na madumu ya vinywaji vya tambiko, nayo mikate, wasiyokoma kumwekea Bwana, sharti iwe juu yake. Kisha na watandaze nguo nyekundu ya kifalme, kisha waifunike kwa blanketi la ngozi za pomboo, kisha na waitie mipiko yake. Kisha na wachukue nguo nyeusi ya kifalme, wakifunike kinara kiangazacho pamoja na taa zake na koleo zake na makato yake na vyombo vyake vyote vya mafuta, wanavyovitumia vya kazi yake. Kisha na wakifunike pamoja na vyombo vyake vyote kwa blanketi la ngozi za pomboo, kisha na wakiweke juu ya miti ya kukichukulia. Kisha watandaze nguo nyeusi ya kifalme juu ya meza ya dhahabu ya kuvukizia, kisha waifunike kwa blanketi la ngozi za pomboo na kuitia mipiko yake. Kisha na wachukue vyombo vyote, wanavyovitumia Patakatifu, wavifunge katika nguo nyeusi ya kifalme na kuvifunika tena kwa blanketi la ngozi za pomboo, kisha waviweke juu ya miti ya kuvichukulia. Kisha na wazoe majivu mezani pa kuteketezea ng'ombe za tambiko, kisha watandaze juu yake nguo nyekundu ya kifalme. Kisha na waweke juu yake vyombo vyake vyote, wanavyovitumia wakifanya kazi za hapo, sinia na nyuma na majembe na vyano na vyombo vyote vya meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, wavifunike juu kwa blanketi la ngozi za pomboo, kisha na waitie mipiko yake. Haroni na wanawe watakapokwisha kupafunika Patakatifu na vyombo vyake vyote wakitaka kuvunja makambi, ndipo, wana wa Kehati watakapoingia kuvichukua, lakini wasiguse vitu vitakatifu, wasife. Hii ndiyo mizigo yao wana wa Kehati, watakayoichukua Hemani mwa Mkutano. Tena kazi yake Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, ni kuyaangalia mafuta ya kinara na mavukizo yanukayo vizuri na vilaji vya tambiko vya kila siku na mafuta ya kupaka, tena kuliangalia Kao lote zima na vyote vilivyomo ndani ya Patakatifu, maana ndivyo vyombo vyake. Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba: Angalieni, shina la udugu wa Wakehati lisitoweke kwao Walawi! Ila yafanyeni haya, wapate kuwapo, wasife, watakapopakaribia Patakatifu Penyewe: Kwanza Haroni na wanawe na waingie, kisha wawaweke kila mtu penye kazi yake na kumpa mzigo wake. Lakini wasiingie kamwe kupatazama tu Patakatifu, ijapo iwe kitambo kidogo kabisa, wsife. Bwana akamwambia Mose kwamba: Fanya hesabu ya wana wa Gersoni nao walio wa milango ya baba zao na wa udugu wao. Uwakague walio wenye miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, ndio wanaofaa wote kuuingia utumishi, wafanye kazi za kutumikia Hemani mwa Mkutano. Hizi ndizo kazi zao walio wa udugu wa Gersoni za kutumika na za kuchukua mizigo: na wayachukue mazulia ya Kao, na Hema la Mkutano na chandalua chake na chandalua cha ngozi za pomboo kilichoko juu yake na pazia la hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, na nguo za uani na pazia la hapo pa kuingia langoni kwa ua, unaolizunguka Kao na meza ya kuteketezea ng'ombe ya tambiko, na kamba zao na vyombo vyote vya utumishi wao, nayo yote yapasayo kufanywa nao na wayafanye. Utumishi wote wa wana wa Gersoni, kama ni kuichukua mizigo iwapasayo yote, au kama ni kuzifanya kazi ziwapasazo zote, ufanyike kwa kuagizwa na Haroni na wanawe; ninyi mwaweke kwa kuzignlia kazi za mizigo yao yote. Hizi ndizo kazi za utumishi wao walio wa udugu wa wana wa Gersoni wa kutumikia Hemani mwa Mkutano, naye atakayewaangalia ni Itamari, mwana wa mtambikaji Haroni. Uwakague nao wana wa Merari walio wa udugu wao wa milango ya baba zao: uwakague walio wa miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, ndio wanaofaa wote kuuingia utumishi, wafanye kazi za kutumikia Hemani mwa Mkutano. Hizi ndizo kazi zao za kuiangalia mizigo yao, nao huo ndio utumishi wao wote wa kufanya Hemani mwa Mkutano: kuzichukua mbao za Kao na misunguo yake na nguzo zake na miguu yake, na nguzo zinazouzunguka au na miguu yao na mambo zao na kamba zao na vyombo vyao vyote, wafanye yote yaupasayo utumishi wao. Navyo vyombo vya kuviangalia, wakivichukua, mwape na kuvitaja kila kimoja jina lake. Hizi ndizo kazi za utumishi wao walio wa udugu wa wana wa Merari, wazifanye za kutumikia Hemani mwa Mkutano, naye mkuu wao awe Itamari, mwana wa mtambikaji Haroni. Kwa hiyo Mose na Haroni na wakuu wa mkutano wakawakagua wana wa Kehati walio wa udugu wao na wa milango ya baba zao; waliokuwa wenye miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, ndio waliofaa wote kuuingia utumishi, wafanye kazi za kutumikia Hemani mwa Mkutano. Jumla yao walio wa udugu wao walikuwa watu 2750. Hii ndiyo jumla yao wote wa udugu wa Wakehati waliotumikia Hemani mwa Mkutano, Mose na Haroni waliowakagua kwa amri, Bwana aliyompa Mose. Wana wa Gersoni wakakaguliwa nao walio wa udugu wao na wa milango ya baba zao, waliokuwa wenye miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, ndio waliofaa wote kuuingia utumishi, wafanye kazi za kutumikia Hemani mwa Mkutano. Jumla yao walio wa udugu wao na wa milango ya baba zao walikuwa watu 2630. Hii ndiyo jumla yao wote wa udugu wa wana wa Gersoni waliotumikia Hemani mwa Mkutano, Mose na Haroni waliowakagua kwa amri ya Bwana. Ndugu za wana wa Merari wakakagulia nao walio wa udugu wao na wa milango ya baba zao, waliokuwa wenye miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, ndio waliofaa wote kuuingia utumishi, wafanye kazi za kutumikia Hemani mwa Mkutano. Jumla yao walio wa udugu wao walikuwa watu 3200. Hii ndiyo jumla yao walio wa udugu wa wana wa Merari, Mose na Haroni waliowakagua kwa amri, Bwana aliyompa Mose. Hawa ndio Walawi wote waliokaguliwa, Mose na Haroni na wakuu wa Waisiraeli waliowakagua, waliokuwa wa udugu wao na wa milango ya baba zao, ndio waliokuwa wenye miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, nao ndio wote waliofaa kufanya kazi za kuutumikia huo utumishi nao utumishi wa kuchukua mizigo Hemani mwa Mkutano. Jumla yao walikuwa watu 8580. Kwa amri, Bwana aliyompa Mose, aliwakagua na kumweka kila mtu mmoja penye kazi yake ya utumishi na penye mzigo wake wa kuuchukua; nao wakawekwa vivyo hivyo, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waagize wana wa Isiraeli, watoe makambini wote walio wenye ukoma nao wote walio wenye kisonono nao wote waliojipatia uchafu kwa kugusa mfu. Sharti mwatoe, kama ni mume au kama ni mke, na kuwatuma kwenda nje ya makambi, wasiyachafue makambi, mimi ninamokaa katikati yao. Wana wa Isiraeli wakayafanya na kuwatuma kwenda nje ya makambi; kama Bwana alivyomwambia Mose, ndivyo, wana wa Isiraeli walivyoyafanya. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waambie wana wa Isiraeli: Mtu mume au mke akifanya kosa lo lote la kimtu na kumvunjia Bwana maagano, mtu huyo atakuwa amekora manza. Hao sharti wayaungame makosa yao, waliyoyafanya, kisha wazilipe manza zao, walizozikora, na kumrudishia mwenyewe, waliyemkosea, mali zake sawasawa na kuongeza fungu la tano. Kama mtu huyo hakuacha ndugu anayepasa kupewa hayo malipo ya manza, sharti Bwana apewe hayo malipo ya manza, yawe yake mtambikaji, wakiisha kutoa humo dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi ya kumpatia upozi. Navyo vipaji vyote vya tambiko, wana wa Isiraeli watakavyovitoa kuwa vitakatifu vya kumnyanyulia Bwana, na wampelekee mtambikaji, navyo vitakuwa vyake. Vipaji vyo vyote, mtu atakavyovitoa kuwa vitakatifu, vitakuwa vyake mtambikaji, navyo vyote, mtu atakavyompa mtambikaji, vitakuwa vyake. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Kama mke wa mtu anakosa na kumvunjia mumewe maagano yake, mtu akilala naye kwa ugoni, vikafichika machoni pa mumewe, asijulikane, ya kuwa amejichafua, kwa kuwa hakuwako shahidi, wala hakufumaniwa, lakini wivu ukiwaka moto rohoni mwake mumee, amwonee mkewe wivu kwa kwamba amejichafua, au pengine wivu ukiwaka moto rohoni mwake mumewe, amwonee mkewe wivu, naye haujichafua, basi, vikiwa hivyo sharti mume ampeleke mkewe kwa mtambikaji pamoja na kumpelekea toleo lake, vibaba viwili vya unga wa mawele, lakini asiumiminie mafuta, wala asiweke uvumba juu yake, kwani ni kilaji cha tambiko cha wivu, tena ni kilaji cha tambiko cha ukumbusho cha kukumbushia manza, alizozikora. Naye mtambikaji na ampeleke huyo mwanamke, amsimamishe mbele yake Bwana, kisha mtambikaji achote maji matakatifu kwa chombo cha udongo, kisha achote hata vumbi kidogo lililoko chini Kaoni, alitie katika hayo maji. Mtambikaji akiisha kumsimamisha huyo mwanamke mbele ya Bwana na kuzifungua nywele za kichwani pake, na ampe mkononi mwake hicho kilaji cha tambiko cha ukumbusho, nacho ni kilaji cha tambiko cha wivu, lakini yale maji machungu yenye maapizo mtambikaji sharti ayashike mkononi mwake. Kisha mtambikaji na amwapishe na kumwambia huyo mwanamke: Kama mtu hakulala kwako, nawe hukukosa na kujichafua ukimtumia mwingine kuwa kama mumeo, hutapatwa na apizo lo lote la haya maji machungu yenye maapizo. Lakini kama umekosa na kujichafua ukimtumia mwingine kuwa kama mumeo, mtu ye yote akilala kwako kwa ugoni asiye mumeo, basi, yatakupata. Kisha mtambikaji na amwapishe huyo mwanamke kwa kiapo cha kuapiza, mtambikaji akimwambia huyo mwanamke: Bwana na akuweke kuwa kielekezo cha kuapizwa katikati yao walio ukoo wako akivipoozesha viuno vyako pamoja na kulivimbisha tumbo lako! Nayo maji haya yenye maapizo na yaingie mwilini mwako, yalivimbishe tumbo lako pamoja na kuvipoozesha viuno vyako! Naye huyo mwanamke sharti aitikie na kusema: Amin. Amin. Kisha mtambikaji na ayaandike haya maapizo chuoni na kuyafuta kwa yale maji machungu. Kisha na amnyweshe huyo mwanamke hayo maji machungu yenye maapizo, yamwingie. Kisha mtambikaji na akichukue kilaji cha tambiko cha wivu mkononi mwa mwanamke, akipitishe motoni mbele ya Bwana na kumtolea mezani pa kutambikia. Hapo mtambikaji na achukue gao moja la kilaji cha tambiko kilicho cha ukumbusho wake mwanamke, akichome moto mezani pa kutambikia, kisha amnyweshe mwanamke yale maji. Akiisha kumnywesha hayo maji, naye akiwa amejichafua na kumvunjia mumewe maagano yake, basi, hayo maji machungu yenye maapizo yatakapomwingia yatalivimbisha tumbo lake pamoja na kuvipoozesha viuno vyake; ndivyo, huyu mwanamke atakavyokuwa ameapizwa kwao walio ukoo wake. Lakini kama mwanamke huyu hakujichafua, akiwa ametakata, hatapatwa na jambo lo lote, ila atazaa watoto tena. Haya ndiyo maonyo yao wenye wivu, mwanamke akiwa amekosa na kujipatia uchafu kwa kutumia mwingine kuwa kama mumewe, au wivu ukiwaka moto rohoni mwa mtu, amwonee mkewe wivu, amsimamishe huyo mwanamke mbele ya Bwana, mtambikaji amfanyizie mambo yote ya haya maonyo. Hapo mumewe atakuwa hana manza zo zote tena, lakini mwanamke aliye hivyo hana budi kujitwika manza, alizozikora. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Mtu mume au mke akitaka kujitenga na kuapa apo la mtu aliyejieua, mtu akitaka kujieua hivyo kuwa wake Bwana, na ajieue kuwa mwenye mwiko wa mvinyo na wa vileo vyo vyote, asinywe wala siki ya mvinyo wala siki ya kileo cho chote, tena asinywe maji ya zabibu, asile zabibu wala mbichi wala kavu. Siku zote za weuo wake asile cho chote kitokacho kwa mzabibu, wala koko wala maganda. Siku zote za maapo ya weuo wake wembe usije kichwani pake; mpaka siku zitimie, alizojieua kuwa wake Bwana, sharti awe mtakatifu na kuziacha nywele za kichwani pake, zikue. Siku zote za kujieua kwake kuwa wake Bwana, asiingie mlimo na mfu. Asijipatie uchafu kwa baba yake, wala kwa mama yake, wala kwa kaka yake, wala kwa mdogo wake, wala kwa umbu lake, wakifa, kwani weuo wa Mungu wake uko kichwani pake. Siku zote za weuo wake ni mtakatifu wa Bwana. Ikiwa, inatukia, asipoviwazia, mara mtu afe hapo alipo, atakuwa amekwisha kukipatia uchafu kichwa chake kilicho na weuo wa Bwana; kwa hiyo sharti azinyoe nywele za kichwani pake siku hiyo, atakapokuwa ametakata, ndio siku ya saba, ndipo azinyoe. Siku ya nane na apeleke huwa wawili au makinda mawili ya njiwa manga kwa mtambikaji hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Mtambikaji na amtumie mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ampatie upozi, kwa kuwa kosa lilimpata hapo penye yule mfu; siku hiyo sharti aseme tena, ya kama kichwa chake ni kitakatifu. Kisha ajieue tena kuwa wake Bwana siku zilezile wa weuo wake na kutoa mwana kondoo wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi; lakini siku zile za kwanza zisihesabiwe, kwa kuwa ule weuo wake ulichafuliwa. Nayo haya ndiyo maongozi yake aliyejieua: siku za weuo wake zitakapotimia, ndipo wampeleke hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Hapo na amtolee Bwana toleo lake: mwana kondoo wa mwaka mmoja asiye na kilema kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima na mwana kondoo jike wa mwaka mmoja asiye na kilema kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo na dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya shukrani, tena kikapu cha mikate isiyochachwa iliyotengenezwa kwa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta, na maandazi membamba yasiyochachwa yaliyopakwa mafuta pamoja na kutoa vilaji na vinywaji vyao vya tambiko. Naye mtambikaji na avipeleke vyote kwa Bwana na kumtolea kwanza ng'ombe yake ya tambiko ya weuo nayo ya kuteketezwa nzima. Kisha na amchinje yule dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya kumshukuru Bwana pamoja na kile kipaji cha mikate isiyochachwa, kisha mtambikaji na avitoe navyo vilaji na vinywaji vyake vya tambiko. Kisha huyu aliyejieua na azinyoe nywele za kichwani pake zilizokuwa na mwiko wa kunyolewa, naye azinyoe hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, kisha na azichukue hizo nywele za kichwani pake zilizokuwa na mwiko wa kunyolea, azitie katika moto unaowaka chini ya ng'ombe ya tambiko ya shukrani. Kisha mtambikaji na achukue mkono wa dume la kondoo uliopikwa, tena mkate mmoja usiochachwa uliomo kikapuni na andazi jembamba moja lisilochachwa, ayaweke mikononi mwake huyo aliyejieua, atakapokwisha kuzinyoa nywele zake za mwiko. Kisha mtambikaji na avipitishe motoni mbele ya Bwana, kwa kuwa vitakatifu ni vyake mtambikaji pamoja na kidari cha kupitishwa motoni na paja la kunyanyuliwa. Kisha huyo aliyejieua atakuwa tena na ruhusa ya kunywa mvinyo. Haya ndiyo maongozi ya mtu atakayejieua na kuapa; haya ndiyo matoleo yake, atakayomtolea Bwana kwa ajili ya weuo wake. Kama yako mengine, mkono wake uwezayo kuyafikisha, ayatoe, basi, na ayatoe; lakini hayo, aliyoyaapa, sharti ayamalize vivyo hivyo, kama alivyoapa, na kuyafuata haya maongozi ya weuo wake. Bwana akamwambia Mose kwamba: Mwambie Haroni na wanawe kwamba: Mkiwabariki wana wa Isiraeli sharti mwaambie hivyo: Bwana akubariki, akulinde! Bwana akuangazie uso wake, akuhurumie! Bwana akuinulie uso wake, akupe utengemano! Watakapowatajia wana wa Isiraeli Jina langu hivi, mimi nitawabriki. Ikawa siku hiyo, Mose alipokwisha kulisimamisha Kao na kulipaka mafuta na kulieua kuwa takatifu pamoja na vyombo vyake vyote na kuipaka mafuta nayo meza ya kutambikia pamoja na vyombo vyake vyote na kuvieua kuwa vitakatifu, ndipo, wakuu wa Waisiraeli waliokuwa vichwa vya milango ya baba zao walipovitoa vipaji vyao vya tambiko, kwa kuwa wakuu wa mashina waliowasimamia wale waliokaguliwa. Wakayaleta hayo matoleo yao, wakatoa mbele ya Bwana magari sita yenye mafuniko na ng'ombe kumi na wawili, kila wakuu wawili wakitoa gari moja, na kila mkuu mmoja akitoa ng'ombe mmoja; hapo mbele ya Kao ndipo, walipoyatoa. Bwana akamwambia Mose kwamba: Yachukue kwao, nayo yatumiwe kuusaidia utumishi wa Hema la Mkutano. Uwape Walawi, kila mtu kama kazi ya utumishi wake ilivyo. Mose akayachukua hayo magari pamoja na ng'ombe, akawapa Walawi. Magari mawili na ng'ombe wanne akawapa wana wa Gersoni kwa hivyo, utumishi wao ulivyokuwa. Magari manne na ng'ombe wanane akawapa wana wa Merari kwa hivyo, utumishi wao ulivyokuwa, Itamari, mwana wa mtambikaji Haroni, aliousimamia. Lakini wana wa Kehati hakuwapa, kwani utumishi wao ulikuwa wa Pataktifu, hawakuwa na budi kuvichukua vyombo vyake mabegani. Kisha wakuu wakatoa vipaji vya weuo wa meza ya kutambikia siku hiyo, ilipopakwa mafuta; ndipo, wakuu walipoyatoa matoleo yao mbele ya meza ya kutambikia. Bwana akamwambia Mose: Kila mkuu mmoja awe na siku yake, nayo hiyo siku yake ndipo kila mkuu mmoja ayatoe matoleo yake ya weuo wa meza ya kutambikia. Aliyeyatoa matoleo yake siku ya kwanza alikuwa Nasoni, mwana wa Aminadabu, wa shina la Yuda. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho ilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Nasoni, mwana wa Aminadabu. Siku ya pili Netaneli, mwana wa Suari, mkuu wa Isakari, akaleta vipaji vyake. Matoleo yake, aliyoyatoa, yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwambamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Netaneli, mwana wa Suari. Siku ya tatu Eliabu, mwana wa Heloni, mkuu wa wana wa Zebuluni, akaleta vipaji vyake. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilukuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Eliabu, mwana wa Heloni. Siku ya nne Elisuri, mwana wa Sedeuri, mkuu wa wana wa Rubeni, akaleta vipaji vyake. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Elisuri, mwana wa Sedeuri. Siku ya tano Selumieli, mwana wa Surisadai, mkuu wa wana wa Simeoni akaleta vipaji vyake. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Selumieli, mwana wa Surisadai. Siku ya sita Eliasafu, mwana wa Deueli, mkuu wa wana wa Gadi, akaleta vipaji vyake. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Eliasafu, mwana wa Deueli. Siku ya saba Elisama, mwana wa Amihudi, mkuu wa wana wa Efuraimu, akaleta vipaji vyake. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Elisama, mwana wa Amihudi. Siku ya nane Gamulieli, mwana wa Pedasuri, mkuu wa wana wa Manase, akaleta vipaji vyake. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima; tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo; tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Gamulieli, mwana wa Pedasuri. Siku ya tisa Abidani, mwana wa Gideoni, mkuu wa wana wa Benyamini, akaleta vipaji vyake. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikukwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Abidani, mwana wa Gideoni. Siku ya kumi Ahiezeri, mwana wa Amisadai, mkuu wa wana wana wa Dani, akaleta vipaji vyake. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo; tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Ahiezeri mwana wa Amisadai. Siku ya kumi na moja Pagieli, mwana wa Okrani, mkuu wa wana wa Aseri, akaleta vipaji vyake. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo wa mwaka mmoja na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Pagieli, mwana wa Okrani. Siku ya kumi na mbili Ahira, mwana wa Enani, mkuu wa wana wa Nafutali, akaleta vipaji vyake. Matoleo yake yalikuwa: bakuli moja ya fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 130, na chano kimoja cha fedha, kiasi chake kilikuwa fedha 70, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu; zote mbili zilikuwa zimejaa unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko; tena kijiko kimoja cha dhahabu, kiasi chake kilikuwa fedha 180, nacho kilikuwa kimejaa mavukizo; tena dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na mwana kondoo mmoja wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, tena dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena ng'ombe wawili na madume matano ya kondoo na wana mbuzi watano na wana kondoo watano wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe za tambiko za shukrani. Haya yalikuwa matoleo yake Ahira, mwana wa Enani. Hivi vilikuwa vipaji, wakuu wa Waisiraeli walivyovitoa vya weuo wa meza ya kutambikia siku hiyo, ilipopakwa mafuta: mabakuli yaa fedha 12 na vyano vya fedha 12 na vijiko vya dhahabu 12. Kila bakuli moja kiasi chake kilikuwa fedha 130, kila chano kimoja kiasi chake kilikuwa fedha 70; jumla ya fedha za hivi vyombo ilikuwa fedha 2400, nazo ni zile fedha zilizotumika Patakatifu. Vijiko vya dhahabu vilivyojaa mavukizo vilikuwa 12, kila kijiko kimoja kiasi chake kilikuwa vipande kumi vya dhahabu, ndio fedha 180; dhahabu zote za hivyo vijiko vilikuwa vipande 120, ndio fedha 2160. Jumla ya ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima ilikuwa: madume 12 ya ng'ombe, mmadume 12 ya kondoo, wana kondoo wa mwaka mmoja 12 pamoja na vilaji vyao vya tambiko; tena madume 12 ya mbuzi kuwa ng'ombe za tambiko za weuo. Nayo jumla ya ng'ombe za tambiko za shukrani ilikuwa: Ng'ombe 24, madume 60 ya kondoo, wana mbuzi 60, wana kondoo 60 wa mwaka mmoja; hivi vilikuwa vipaji vya weuo wa meza ya kutambikia, ilipokwisha kupakwa mafuta. Kisha kila mara Mose alipoingia Hemani mwa Mkutano kusema na Bwana alisikia, sauti yake ikisema naye toka hapo penye Kiti cha Upozi kilicholifunika Sanduku la Ushahidi, nayo ilitoka katikati ya Makerubi, ikasema naye. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na Haroni na kuwambia: Utakapoziweka taa juu ya kinara, uangalie, hizi taa zote saba ziangaze mahali pale palipo mbele ya kinara. Haroni akafnya hivyo; alipoziweka hizo taa, huangalia, ziangaze mahali palipo mbele ya kinara, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Nacho kinara kilikuwa kimetengenezwa kwa kufua dhahabu; toka shina lake hata maua yake, yote pia ilikuwa kazi ya kufuafua dhahabu; kama ule mfano ulivyokuwa, Bwana aliomwonyesha Mose, ndivyo, walivyokitengeneza hicho kinara. Bwana akamwambia Mose kwamba: Wachukue Walawi na kuwatoa katikati ya wana wa Isiraeli, upate kuwatakasa. Nawe uwafanyizie hivyo ukiwatakasa: wanyunyizie maji ya weuo, nao na wajinyoe kwa wembe miili yao yote mizima, kisha na wazifue nguo zao, wapate kutakata. Kisha na wachukue dume la ng'ombe aliye kijana bado pamoja na kilaji chake cha tambiko, ndio unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta. Nawe uchukue dume jingine la ng'ombe aliye kijana bado kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. Kisha wapeleke Walawi, wafike mbele ya Hema la Mkutano, ukiwakusanya nao wote walio wa mkutano wa wana wa Isiraeli. Kisha watokeze Walawi usoni pa Bwana, wana wa Isiraeli wakiwabandikia Walawi mikono yao. Naye Haroni na awapitishe Walawi mbele ya Bwana huku na huko, wawe kipaji cha tambiko, wana wa Isiraeli walichokitoa cha kupitishwa motoni mbele ya Bwana, wapate kuutumikia utumishi wa Bwana. Kisha Walawi na waibandike mikono yao vichwani pao wale ng'ombe, kisha umtumie mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili kuwa ng'ombe ya tambiko ya Bwana ya kuteketezwa nzima, uwapatie Walawi upozi. Kisha wasimamishe Walawi mbele ya Haroni na mabele ya wanawe na kuwapitishwa mbele ya Bwana huku na huko, wawe kipaji cha tambiko cha kupitishwa motoni. Ndivyo, utakavyowatenga Walawi na kuwatoa katikati ya wana wa Isiraeli, Walawi wapate kuwa wangu. Baadaye Walawi na waingie kulitumikia Hema la Mkutano. Hivyo ndivyo, utakavyowatakasa na kuwapitisha huku na huko mbele ya Bwana, wawe kipaji cha tambiko cha kupitishwa motoni. Kwani hawa ndio niliopewa, watolewe katikati ya wana wa Isiraeli kuwa makombozi ya watoto wote wa kiume watakaozaliwa wa kwanza na mama zao; mahali pao hao wana wote wa kwanza nimewachukua wao kwa wana wa Isiraeli kuwa wangu. Kwani kila mwana wa kwanza kwao wana wa Isiraeli ni wangu, kama ni wa mtu au wa nyama wa kufuga tangu siku ile, nilipowapiga wana wa kwanza wote katika nchi ya Misri; ndivyo, nilivyowatakasa, wawe wangu, nikiwachukua Walawi kuwa makombozi ya wana wote wa kwanza kwao wana wa Isiraeli. Nami hawa Walawi nikiwapa Haroni na wanawe, wawe kipaji chao kilichotolewa katikati yao wana wa Isiraeli, wautumikie utumishi wao wana wa Isiraeli wa Hemani mwa Mkutano na kuwapatia wana wa Isiraeli upozi, hao wana wa Isiraeli wasipatwe na pigo lo lote, wao wana wa Isiraeli wakilikaribia Hema la Mkutano. Kwa hiyo Mose na Haroni nao wote waliokuwa wa mkutano wa wana wa Isiraeli wakawafanyizia Walawi yote sawasawa, kama Bwana alivyomwagiza Mose kuwafanyizia Walawi; hivyo ndivyo, wana wa Isiraeli walivyowafanyizia. Walawi walipokwisha kujieua na kuzifua nguo zao, Haroni akawapitisha huku na huko mbele ya Bwana, kisha Haroni akawapatia upozi kwa hivyo, alivyowatakasa. Baadaye Walawi wakaingia kuutumikia utumishi wa Hemani mwa Mkutano machoni pa Haroni napo machoni pa wanawe; kama Bwana alivyomwagiza Mose kuwafanyizia Walawi, ndivyo, walivyowafanyizia. Bwana akamwambia Mose kwamba: Hii ndiyo inayowapasa Walawi: tangu hapo, mtu alipopata miaka 25 na zaidi na aingie zamu ya utumishi wa Hemani mwa Mkutano. Lakini tangu hapo, mtu anapopata miaka 50 na atoke katika zamu ya utumishi huo, asiutumikie tena. Wataweza kuwasaidia ndugu zao mle Hemani mwa Mkutano na kulinda ulinzi, lakini kazi za utumishi wasizifanye. Hivyo ndivyo, utakavyowafanyizia Walawi, waziangalie kazi zao. Bwana akamwambia Mose nyikani kwa Sinai katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili tangu hapo, walipotoka katika nchi ya Misri kwamba: Wana wa Isiraeli na waitengeneze kondoo ya Pasaka, siku zake zilizowekwa zitakapotimia. Siku ya kumi na nne ya huu mwezi wakati wa jioni mwitengeneze saa zizo hizo zilizowekwa, myafuate maongozi yake yote na desturi zake zote zipasazo. Mwitengeneze vivyo hivyo. Kwa hiyo Mose akawaambia wana wa Isiraeli, waitengeneze kondoo ya Pasaka. Nao wakaitengeneza kondoo ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza wakati wa jioni kule nyikani kwa Sinai; yote, Bwana aliyomwagiza Mose, wana wa Isiraeli wakayafanya vivyo hivyo sawasawa. Wakawako watu waliokuwa wenye uchafu kwa ajili ya kufiwa; kwa hiyo hawakuweza kuitengeneza kondoo ya Pasaka siku hiyo, wakamtokea Mose na Haroni siku hiyo. Hao watu wakawaambia: Sisi tu wenye uchafu kwa ajili ya kufiwa; mbona tunakatazwa kumtolea Bwana matoleo katikati ya wana wa Isiraeli siku hiyo iliyowekwa? Mose akawaambia: Ngojeni, nisikie, Bwana atakayoyaagiza kwa ajili yenu. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waambie wana wa Isiraeli kwamba: Kila mtu wa kwenu au wa vizazi vyenu, kama ni mwenye uchafu kwa kufiwa au kama yuko mbali safarini, naye ataweza kuitengeneza kondoo ya Pasaka ya Bwana. Na aitengeneze siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili wakati wa jioni, tena na waile pamoja na mikate isiyochachwa na mboga zenye uchungu. Lakini wasisaze nyama mpaka kesho, tena watu wasivunje mifupa, ila waile na kuyafuata maongozi yote ya Pasaka. Lakini mtu asipokuwa mwenye uchafu, wala asipokuwa safarini, akiacha tu kuitengeneza kondoo ya Pasaka, mtu aliye hivyo sharti ang'olewe kwao walio ukoo wake, kwani hakumtolea Bwana matoleo siku hiyo iliyowekwa. Mtu aliye hivyo sharti atwikwe kosa lake. Kama kwenu atakuwako mgeni, naye akitaka kuitengeneza kondoo ya Pasaka ya Bwana, basi, na aitengeneze na kuyafuata maongozi ya Pasaka na desturi zake ziipasazo; maongozi ya kwenu yawe yaleyale, nayo huwapasa wageni na wenyeji wa nchi hiyo. Siku hiyo, walipolisimamisha Kao, lile wingu likalifunika Kao kuwa juu yake Hema la Ushahidi; lakini jioni likaonekana juu ya Kao kuwa kama moto mpaka asubui. Vikawa hivyo siku zote: hilo wingu lililifunika Kao, tena usiku likaonekana kuwa kama moto. Napo, hilo wingu lilipoondoka penye Hema, likiisha, ndipo, wana wa Isiraeli walipoondoka kwenda safari yao; napo mahali, hilo wingu lilipotua, ndipo, wana wa Isiraeli walipopiga makambi. Hivyo wana wa Isiraeli waliondoka kusafiri kwa kuagizwa na Bwana, tena kwa kuagizwa na Bwana walipiga makambi. Siku zote, hilo wingu lilipokaa juu ya Kao, nao walikaa makambini. Napo hapo, wingu lilipokawilia na kukaa siku nyingi juu ya Kao, wana wa Isiraeli wakamwangalia Bwana, kama ilivyowapasa kumwangalia, lakini hawakuondoka kwenda safari yao. Wingu lilipokuwa juu ya Kao siku chache tu, walikaa makambini kwa kuagizwa na Bwana; tena kwa kuagizwa na Bwana waliondoka kwenda safari yao. Wingu lilipokaa tu toka jioni hata asubuhi, kisha wingu lilipoondoka asubuhi, nao waliondoka kwenda safari yao; au lilipokaa tu mchana na usiku pamoja, basi, hapo wingu lilipoondoka, nao waliondoka kwenda safari yao. Lakini wingu lilipokaa juu ya Kao siku mbili au mwezi au siku nyingi zaidi, nao wana wa Isiraeli walikaa makambini, hawakuondoka kwenda safari yao; lakini lilipoondoka, nao waliondoka kwenda safari yao. Hivyo walikaa makambini kwa kuagizwa na Bwana, tena waliondoka kwenda safari yao kwa kuagizwa na Bwana. Ndivyo, walivyomwangalia Bwana, kama ilivyowapasa kuyaangalia, Bwana atakayoyaagiza kinywani mwa Mose. Bwana akamwambia Mose kwamba: Jifanyizie matarumbeta mawili ya fedha, nayo uyatengeneze kwa kufuafua fedha, uyatumie kuwa ya kuwaitia wao wa mkutano, tena ya kuwatangazia, wavunje makambi. Yatakapopigwa yote mawili, watu wote wakusanyike kwako hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Lakini litakapopigwa moja tu, na wakusanyike kwako wakuu tu walio vichwa vyao maelfu ya Waisiraeli. Lakini mtakapoyapiga kwa sauti kuu za kushangilia, makambi yaliyoko upande wa maawioni kwa jua na yavunjwe. Mtakapoyapiga mara ya pili kwa sauti kuu za kushangilia, makambi yaliyoko upande wa kusini na yavunjwe. Yatakapopigwa kwa sauti kuu za kushangilia yatakuwa ya kuvunjia makambi. Lakini kwa kuukusanya mkutano mtayapiga tu pasipo kuzitumia sauti kuu za kushangilia. Nao wana wa Haroni walio watambikaji ndio watakaoyapiga hayo matarumbeta. Haya na yawe maongozi ya kale na kale kwenu na kwa vizazi vyenu. Napo hapo, mtakapokwenda vitani katika nchi yenu kupigana na adui watakaowasonga, na mshangilie na kuyapiga hayo matarumbeta; ndipo, mtakapokumbukwa mbele ya Bwana Mungu wenu, mwokolewe katika adui zenu. Nazo siku za furaha zenu na za sikukuu zenu na za miandamo ya mwezi na myapige, mkizitoa ng'ombe zenu za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani; ndipo, yatakaposaidia, mkumbukwe mbele ya Mungu wenu. Mimi Bwana ni Mungu wenu. Ikawa siku ya ishirini ya mwezi wa pili katika mwaka wa pili, ndipo, lile wingu lilipoondoka penye Kao la Ushahidi. Nao wana wa isiraeli wakaondoka kwenda safari yao na kutoka nyikani kwa Sinai, nalo wingu likatua tena katika nyika ya Parani. Kama Bwana alivyoviagiza kinywani mwa Mose, ndivyo, wa kwanza walivyoondoka. Kwanza ikaondoka bendera ya makambi ya wana wa Yuda, vikosi kwa vikosi, naye mkuu wa vikosi vyao alikuwa Nasoni, mwana wa Aminadabu. Naye mkuu wa shina la wana wa Isakari alikuwa Netaneli, mwana wa Suari. Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Zebuluni alikuwa Eliabu, mwana wa Heloni. Kisha Kao likashushwa, nao wana wa Gersoni na wana wa Merari wakaondoka na kulichukua Kao. Kisha bendera ya makambi ya Rubeni ikaondoka, vikosi kwa vikosi, naye mkuu wa vikosi vyao alikuwa Elisuri, mwana wa Sedeuri. Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Simeoni alikuwa Selumieli, mwana wa Surisadai. Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Gadi alikuwa Eliasafu, mwana wa Deueli. Kisha wakaondoka Wakehati wakivichukua vyombo vitakatifu; hao walipofika, wale walikuwa wamekwisha kulisimamisha Kao. Kisha bendera ya makambi ya wana wa Efuraimu ikaondoka, vikosi kwa vikosi, naye mkuu wa vikosi vyao alikuwa Elisama, mwana wa Amihudi. Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Manase alikuwa Gamulieli, mwana wa Pedasuri. Nye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Benyamini alikuwa Abidani, mwana wa Gideoni. Kisha bendera ya makambi ya wana wa Dani ikaondoka, vikosi kwa vikosi; nao walikuwa wanyuma wa makambi yote, naye mkuu wa vikosi vyao alikuwa Ahiezeri, mwana wa Amisadai. Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Aseri alikuwa Pagieli, mwana wa Okrani. Naye mkuu wa vikosi vya shina la wana wa Nafutali alikuwa Ahira, mwana wa Enani. Hivyo ndivyo, wana wa Isiraeli walivyokwenda safarini, vikosi kwa vikosi, walipoondoka kwenda safari yao. Mose akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli wa Midiani, mkwewe Mose: Sisi tunaondoka kwenda mahali, Bwana aliposema: Hapo ndipo, nitakapowapa ninyi; nenda pamoja nasi, tutakufanyizia mema, kwani Bwana amewaambia wana wa Isiraeli, ya kuwa atawapa mema. Lakini akamwambia: Sitakwenda, ila nitarudi kwetu kwa ndugu zangu wa kuzaliwa nao. Akamjibu: Usituache! Kwa kuwa unajua mahali, tunapoweza kupiga makambi nyikani, kwa hiyo utakuwa kama macho yetu sisi. Ukienda na sisi, tutakufanyizia mema yote, Bwana atakayotufanyizia sisi. Walipoondoka mlimani kwa Bwana, wakasafiri siku tatu, nalo Sanduku la Agano la Bwana likawatangulia safari ya hizo siku tatu, liwatafutie mahali pa kupumzikia. Nalo wingu la Bwana lilikuwa juu yao mchana, walipoondoka makambini. Kila mara Sanduku lilipoondoka, Mose akasema: Inuka, Bwana, adui zako watawanyike, nao wachukivu wako waukimbie uso wako! Tena lilipotua husema: Rudi, Bwana, kwenye maelfu na maelfu ya Isiraeli! Lakini watu wakanuna, vikawa vibaya masikioni mwa Bwana; naye Bwana alipovisikia, makali yake yakawaka moto, nao moto wa Bwana ukawawakia, ukayala makambi yaliyokuwa pembeni. Ndipo, watu walipomlilia Mose; naye Mose alipomlalamikia Bwana, moto ukakoma. Wakapaita mahali pale Tabera (Wakio la Moto), kwa kuwa moto wa Bwana uliwawakia hapo. Wafuasi waliokuwa katikati yao wakaingiwa na tamaa kabisa; ndipo, nao wana wa Isiraeli walipolia tena na kusema: Yuko nani atakayetupa nyama, tule? Tunazikumbuka samaki, tulizokula bure tu katika nchi ya Misri, nayo matango na matikiti na mabogaboga na vitunguu na vitunguu somu. Lakini sasa roho zetu zimekauka, kwani hivyo vyote haviko, macho yetu huona Mana tu. Nazo Mana zilikuwa kama punje za mtama mweupe, tena ukizitazama zilifanana na magwede. Watu wakazungukazunguka na kuziokota, wakazisaga kwa mawe ya kusagia, au wakazitwanga katika vinu, kisha wakazipika katika nyungu au wakatengeneza mikate, nayo walipoila ilikuwa kama maandazi penye mafuta matamu. Umande ulipoanguka usiku makambini, Mana nazo zikaanguka pamoja nao. Mose alipowasikia watu, wakilia ndugu na ndugu pamoja, kila mtu pa kuliingilia hema lake, nayo makali ya Bwana yalipowaka sana, vikawa vibaya machoni pake Mose. Kwa hiyo Mose akamwambia Bwana: Mbona unamfanyizia mtumishi wako vibaya? Mbona sioni upendeleo machoni pako? Mbona unanitwika mizigo ya watu hawa wote? Je? Aliyewazaa watu hawa wote kwa kuwachukua mimba ni mimi? Unaniambiaje: Wachukue kifuani pako, kama mnyonyeshaji anavyobeba mtoto mchanga, uwapeleke katika nchi, uliyowaapia baba zao kuwapa? Nitoe wapi nyama za kuwapa hao watu wote? Kwani wananililia kwamba: Tupe nyama, tule! Mimi peke yangu siwezi kuwatunza watu hawa wote, ni mzigo unaonilemea na kunishinda. Ukitaka kunifanyizia hivi, niue kabisa, kama nimeona upendeleo machoni pako, nisiendelee kuyaona haya mabaya yaliyonipata. Bwana akamwambia Mose: Toa katika wazee wa Waisiraeli watu 70, uwakusanye kwangu, nao wawe watu, unaowajua, ya kuwa ndio wazee wa watu walio wenye amri, uwapeleke penye Hema la Mkutano, wajipange hapo pamoja na wewe. Nami nitashuka, niseme hapo na wewe, nayo roho inayokukalia nitaichukua nusunusu na kuiweka juu yao, wajitwike pamoja na wewe mzigo wa kuwatunza watu hawa, usiuchukue peke yako tena. Nao watu hawa waambie: Jitakaseni kuwa tayari kesho, mpate nyama! Kwani mmelia masikioni mwa Bwana kwamba: Yuko nani atakayetupa nyama, tule? kwani huko Misri tuliona mema. Bwana ndiye atakayewapa nyama, mle. Nanyi hamtazila siku moja tu wala siku mbili wala siku tano wala siku kumi wala siku ishirini, ila na mzile mwezi mzima, hata zitoke puani mwenu, hata ziwatapishe, kwa kuwa mmemkataa Bwana anayekaa katikati yenu, mlipomlilia kwamba: Kwa nini tumetoka Misri? Mose akasema: Watu hawa, nilio nao hapa, ni watu 600000 wanaokwenda kwa miguu, nawe unasema: Nitawapa nyama, wale mwezi mzima! Je? Itawezekana kuwachinjia kondoo na mbuzi na ng'ombe, wapate nyama za kutosha? Au inawezekana kuwakusanyia samaki wote wa baharini, wapate samaki nazo za kutosha? Ndipo, Bwana alipomwambia Mose: Je? Mkono wa Bwana umegeuka kuwa mfupi? Sasa utaona, kama neno langu linakupatia kitu, au kama ni la bure. Kisha Mose akatoka, akawaambia watu hayo maneno ya Bwana; akatoa katika wazee wa Waisiraeli watu 70, akawakusanya, akawapanga, walizunguke Hema. Ndipo, Bwana aliposhuka winguni kusema naye, nayo roho iliyomkalia akaichukua nusunusu, akawagawia hao wazee 70; ikawa, roho ilipotua juu yao, ndipo, walipofumbua mambo, lakini hawakuendelea. Kulikuwa na watu wawili waliosalia makambini, mmoja jina lake Eldadi, wa pili jina lake Medadi, nao roho ikatua juu yao, kwani walikuwa wameandikwa, lakini hawakutokea Hemani, nao wakafumbua mambo makambini. Ndipo, kijana alipopiga mbio kumpasha Mose habari kwamba: Eldadi na Medadi wamo makambini wakifumbua mambo. Yosua, mwana wa Nuni, aliyekuwa mtumishi wake Mose tangu ujana wake, akajibu na kusema: Bwana wangu Mose, wakomeshe! lakini Mose akamwambia: Wewe unaona wivu kwa ajili yangu mimi? Laiti watu wote wa Bwana wangekuwa wafumbuaji, Bwana akiwagawia roho yake! Kisha Mose akarudi tena makambini yeye pamoja na hao wazee wa Waisiraeli. Ndipo, upepo ulipotoka kwake Bwana, ukatoa tombo upande wa baharini, ukawatawanya po pote penye makambi, kupita katikati yao ulikuwa mwendo wa siku moja upande wa huku, nao upande wa huko ulikuwa mwendo wa siku moja, vivyo hivyo kuyazunguka makambi yote, tena juu ya nchi ilikuwa mikono miwili kuupima wingi wao. Watu wakaondoka, wakawa wakiwaokota hao tombo mchana kutwa na usiku kucha, tena mchana wa kesho; aliyeokota machache aliokota frasila mia, wakawaanika pande zote za kuyazunguka makambi. Lakini nyama zilipokuwa zingaliko vinywani mwao, zilipokuwa hazijaisha kutafunwa, ndipo, makali ya Bwana yalipowawakia hao watu, naye Bwana akawapiga hao watu pigo kubwa mno. Kwa hiyo walipaita mahali pale Makaburi ya uchu, kwa kuwa walizika hapo watu waliouawa na Uchu mwingi. Watu walipoondoka hapo penye Makaburi ya Uchu wakaenda Haseroti, wakakaa Haseroti. Miriamu na Haroni wakamteta Mose kwa ajili ya mke wa Kinubi, aliyemwoa; kwani Mose alioa mwanamke wa Kinubi. Wakasema: Je? Bwana alisema na Mose peke yake tu? Hakusema na sisi nasi? Naye Bwana akayasikia. Lakini Mose alikuwa mtu mpole sana kuliko watu wote walioko huku nchini. Mara Bwana akamwambia Mose, nao Haroni na Miriamu: Tokeni ninyi watatu, mfike penye Hema la Mkutano! Ndipo, walipotoka wao watatu. Bwana akashuka katika lile wingu lililokuwa kama nguzo, akasimama hapo pa kuliingilia Hema, akamwita Haroni na Miriamu, nao wakatokea wote wawili. Akasema: Yasikieni maneno yangu! kama kwenu yuko mfumbuaji, mimi Bwana nitajijulisha kwake kwa maono, niseme naye kwa ndoto. Lakini vya mtumishi wangu Mose sivyo vilivyo, kwani yeye ni mwelekevu katika nyumba yangu yote nzima. Nasema naye kinywa kwa kinywa, naye huniona mimi Bwana, nilivyo, haoni kivulivuli tu au mfano tu; kwa nini ninyi hamkuogopa kuteta na mtumishi wangu Mose? Makali ya Bwana yakawawakia, naye akaenda zake, nalo wingu likaondoka juu ya Hema; walipotazama, Miriamu alikuwa mwenye ukoma uliokuwa mweupe kama chokaa juani. Haroni naye alipomgeukia Miriamu akamwona, ya kuwa ni mwenye ukoma. Ndipo, Haroni alipomwambia Mose: E Bwana wangu, usitutwike hilo kosa letu, tulilolikosa kwa upumbavu! Huyu umbu letu asiwe kama mfu aliyekwisha kuliwa nusu ya nyama za mwili wake hapo, alipotoka tumboni mwa mama yake. Mose akamlilia Bwana kwamba: E Mungu, ninakuomba sana, umponye. Bwana akamwambia Mose: Kama baba yake angalimtemea mate usoni pake, hangaliona soni siku saba? Na afungiwe siku saba nje ya makambi, baadaye na arudishwe tena. Kwa hiyo Miriamu akafungiwa nje ya makambi siku saba, nao watu hawakuondoka kwenda safari yao, mpaka Miriamu akarudishwa. Kisha watu wakaondoka Haseroti kwenda safari yao, wakapiga makambi katika nyika ya Parani. Bwana akamwambia Mose kwamba: Tuma watu kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani, mimi ninayotaka kuwapa wana wa Isiraeli. Kila shina la baba zao na litoe mtu mmoja, mtakayemtuma, nao wote wawe wakuu kwao. Kwa kuagizwa na Bwana Mose akawatuma kutoka kule nyikani kwa Parani, nao watu hao wote walikuwa vichwa vya wana wa Isiraeli. Nayo haya ndiyo majina yao: wa shina la Rubeni Samua, mwana wa Zakuri, wa shina la Simeoni Safati, mwana wa Hori, wa shina la Yuda Kalebu, mwana wa Yefune, wa shina la Isakari Igali, mwana wa Yosefu, wa shina la Efuraimu Hosea, mwana wa Nuni, wa shina la Benyamini Palti, mwana wa Rafu, wa shina la Zebuluni Gadieli, mwana wa Sodi, wa shina la Yosefu wa shina la Manase Gadi, mwana wa Susi, wa shina la Dani Amieli, mwana wa Gemali, wa shina la Aseri Seturi, mwana wa Mikaeli, wa shina la Nafutali Nabi, mwana wa Wofusi, wa shina la Gadi Gueli, mwana wa Maki. Haya ndiyo majina ya wale watu, Mose aliowatuma kuipeleleza nchi. Lakini Hosea, mwana wa Nuni, Mose akamwita Yosua. Mose alipowatuma kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani akawaambia: Pandeni huku kusini, kisha mpande milimani. Mwitazame hiyo nchi, ilivyo, nao watu wanaokaa huko, kama ni wanguvu, au kama ni wanyonge, kama ni wachache, au kama ni wengi. Itazameni hiyo nchi, wale watu wanayoikaa, kama ni jema, au kama ni mbaya, nayo miji, wale watu wanayoikaa, itazameni, itazameni, kama ni makambikambi tu, au kama ni miji yenye maboma. Nchi itazameni, kama ni yenye wiva, au kama haizai, kama iko miti, au kama hakuna. Tena jipeni mioyo, mchukue matunda ya nchi hiyo! Nazo siku zile zilikuwa siku za malimbuko ya mizabibu. Kisha wakaenda kupanda huko, wakaipeleleza nchi toka nyika ya Sini mpaka Rehobu kwenye njia ya kwenda Hamati. Kisha wakapanda upande wa nchi ya kusini, wakafika Heburoni; ndiko, walikokaa Ahimani, Sesai na Talmai, wana wa Anaki. Nao Heburoni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri. Walipofika penye kijito cha Eskoli, wakakata huko tawi la mzabibu lenye kichala, wakalichukua mpikoni watu wawili, wakachukua hata komamanga na kuyu. Mahali pale wakapaita Kijito cha Eskoli (Kichala) kwa ajili ya hicho kichala, wana wa Isiraeli walichokikata huko. siku 40 zilipopita, wakarudi, kwa kuwa walikwisha kuipeleleza hiyo nchi. Wakaja, wakafika kwa Mose na Haroni na kwa mkutano wote wa wana wa Isiraeli katika nyika ya Parani kule Kadesi, wakawasimulia wao nao mkutano wote waliyoyaona, wakawaonyesha nayo yale matunda ya hiyo nchi. Wakawasimulia kwamba: Tumeiingia nchi, mliyotutuma, ichuruzikayo maziwa na asali, nayo haya ni matunda yake. Lakini wale wanaokaa katika hiyo nchi wako na nguvu, nayo miji yao ni mikubwa sana yenye maboma magumu; nao wana wa Anaki tumewaona huko. Waamaleki wanakaa katika nchi ya kusini; nao Wahiti na Wayebusi na Waamori wanakaa milimani, nao Wakanaani wanakaa upande wa baharini na kando ya Yordani. Naye Kalebu akawatuliza mioyo wale watu mbele ya Mose akisema: Haya! Na tupande, tuichukue hiyo nchi! Kwani tutaweza kuishinda kabisa. Lakini wale watu wengine waliopanda naye wakasema: Hatuwezi kupanda, tupigane na hao watu, kwani ndio wenye nguvu kuliko sisi. Wakazidi kuisingizia nchi ile, waliyoipeleleza, wakiwaambia wana wa Isiraeli: Hiyo nchi, tuliyoipita kuipeleleza, ndiyo nchi inayowala wenyeji wake, nao watu wote, tuliowaona huko, ni watu warefu mno. Huko tumeona hata wale Majitu, ni wana wa Anaki wa mlango wa hao Majitu, nasi tukawa machoni petu kama panzi, tena ndivyo, tulivyokuwa machoni pao. Ndipo, wao wote wa mkutano walipozipaza sana sauti zao, watu wakalia usiku kucha. Wana wote wa Isiraeli wakamnung'unikia Mose na Haroni, nao wote walio wa mkutano wao wakawaambia: Afadhali tungalikufa katika nchi ya Misri au tungekufa huku nyikani! Kwa nini Bwana anatupeleka katika nchi ile, tuuawe kwa panga, wake zetu nao watoto wetu watekwe? Haitatufalia zaidi kurudi Misri? Wakasemezana wao kwa wao: Na tujipatie mkuu, turudi Misri? Ndipo, Mose na Haroni walipojiangusha nyusoni pao mbele ya huo mkutano wote wa wana wa Isiraeli uliokusanyika. Nao Yosua, mwana wa Nuni, na Kalebu, mwana wa Yefune, waliokuwa pamoja nao walioipeleleza hiyo nchi, wakayararua mavazi yao, wakauambia mkutano wote wa wana wa Isiraeli kwamba; Ile nchi, tuliyoipita na kuipeleleza, ni nchi njema sanasana. Bwana akipendezwa nasi, atatuingiza katika nchi hiyo, atupe, iwe yetu; nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali. Ni hili tu, msimpingie Bwana! Tena wale watu wa nchi hiyo msiwaogope, kwani watakuwa kama chakula chetu, nacho kivuli, walichokikimbilia, kimeondoka kwao, naye Bwana yuko pamoja na sisi, kwa hiyo msiwaogope! Wao wote wa huo mkutano walipotaka kuwaua na kuwatupia mawe, ndipo, utukufu wa Bwana ulipotokea penye Hema la Mkutano mbele ya wana wote wa Isiraeli. Bwana akamwambia Mose: Watu hawa watanitukana mpaka lini? Watakataa mpaka lini kunitegemea? Nami nimevifanya hivyo vielekezo vyote kwao! Nitawapiga kwa ugonjwa mbaya uuao, niwatoweshe, kisha nitakufanya wewe kuwa kabila kubwa lenye nguvu kuliko hawa. Lakini Mose akamwambia Bwana: Wamisri watavisikia; kwani wewe umewatoa watu hawa kwa nguvu yako katikati yao, ukawaleta huku. Nao wenyeji wa nchi hii watasimuliwa, kwani nao wamesikia, ya kuwa wewe Bwana uko katikati ya watu hawa, uliowatokea, wakuone macho kwa macho wewe Bwana, tena ya kuwa wingu lako huwasimamia, ukiwatangulia mchana kwa wingu linalofanana na nguzo, nao usiku kwa wingu le moto linalofanana na nguzo Kama ungewaua watu hawa kama mtu mmoja, ndipo, wamizimu waliousikia uvumi wako watakaposema kwamba: Kwa kuwa Bwana hakuweza kuwaingiza watu hawa katika nchi hiyo, aliyoiapia kuwapa, kwa hiyo amewachinja nyikani. Sasa nguvu ya Bwana wangu na ionekane kuwa kuu, kama ulivyosema kwamba: Bwana ni mwenye uvumilivu na upole mwingi, huondoa manza na mapotovu, lakini mbele yake hakuna asiye mkosaji; nazo manza, baba walizozikora, huzilipisha wtoto, akifikishe kizazi cha tatu na cha nne. Waondolee watu hawa manza kwa ukubwa wa upole wako, kama ulivyowaondolea watu hawa makosa yao kutoka Misri mpaka hapa! Ndipo, Bwana aliposema: Nimewaondolea makosa kwa hivyo, ulivyowaombea. Kwa hivyo, nilivyo Mwenye uzima, ulimwengu wote utaenezwa utukufu wangu. Kwani watu hawa wote waliouona utukufu wangu na vielekezo vyangu, nilivyovifanya Misri na nyikani, wakanijaribu sana mara kumi wakikataa kuisikiliza sauti yangu, hawa wote hawataiona nchi, niliyowaapia baba zao kuwapa, kweli wao wote walionitukana hawataiona kabisa. Ni mtumishi wangu Kalebu tu aliye mwenye roho nyingine moyoni mwake, akanifuata kwa moyo wote, basi, yeye nitamwingiza katika nchi hiyo, aliyoiingia kwanza, nao wa uzao wake wataichukua kuwa yao, lakini Waamaleki na Wakanaani watakaa bondeni. Kesho geukeni na kujiendea nyikani mkishika njia ya kwenda kwenye Bahari Nyekundu. Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba: Itakuwa mpaka lini, watu wa mkutano huu mbaya wakininung'unikia? Nimeyasikia manung'uniko ya wana wa Isiraeli, wao waliponinung'unikia. Waambie: Ndivyo, asemavyo Bwana: Kwa hivyo, nilivyo Mwenye uzima, nitawafanyizia yayo hayo, mliyoyasema masikioni mwangu: Huku nyikani itaanguka mizoga yenu ninyi nyote mliokaguliwa na kuhesabiwa, mlio wenye miaka ishirini na zaidi, mlioninung'unikia. Ninyi nyote hamtaiingia kabisa ile nchi, niliyoiapia na kuuinua mkono wangu, ya kwamba nitawakalisha huko. Kalebu, mwana wa Yefune, na Yosua, mwana wa Nuni, hawa tu wataiona. Lakini watoto wenu, mliowasema, ya kama watakuwa mateka, nitawaingiza huko waijue nchi ile, mliyoikataa. Lakini mizoga yenu ninyi itaanguka huku nyikani. Lakini kwanza wana wenu watakuwa wachungaji nyikani miaka 40, watwikwe ugoni wenu, mpaka mizogo yenu imalizike nyikani. Kwa hesabu ya zile siku 40, mlizoipeleleza ile nchi, kila siku moja itahesabiwa kuwa mwaka mmoja; hivyo ndivyo, watakavyotwikwa miaka 40 manza, mlizozikora, mpate kutambua, mambo yanavyoendelea, nikiondoka kwenu. Mimi Bwana nimesema, nami nitawafanyizia haya wao wote walio wa mkutano huu mbaya waliokusanyika, wanipingie: huku nyikani watamalizika, kwani huku ndiko, watakakofia. Kisha wale watu, Mose aliowatuma kuipeleleza nchi ile, ni wao waliounung'unisha mkutano wote waliporudi na kutoa habari za nchi ile, hao watu waliozitoa zile habari mbaya za nchi ile wakafa kwa kupigwa na Bwana. Lakini Yosua, mwana wa Nuni, na Kalebu, mwana wa Yefune, ndio waliokaa wenye uzima miongoni mwao waliokwenda kuipeleleza ile nchi. Mose alipowaambia wana wote wa Isiraeli maneno haya, wakasikitika sana. Kesho yake wakaamka na mapema, wakapanda mlimani juu kileleni na kusema: Basi, tumekwisha kufika huku, sasa twende kupanda mahali pale, Bwana alipotuelekeza! Kwani tumekosa. Lakini Mose akasema: Mbona ninyi mwataka kuitangua amri ya Bwana? Hamtafanikiwa. Msipande! Kwani Bwana hamnaye katikati yenu, msipigwe na adui zenu. Kwani Waamaleki na Wakanaani wako mbele yenu, nanyi mtaangushwa kwa panga, kwa kuwa mmerudi nyuma na kumwacha Bwana; kwa hiyo Bwana hatakuwa nanyi. Lakini kwa kujivuna wakapanda mlimani juu kileleni, lakini Sanduku la Agano la Bwana na Mose hawakutoka makambini. Ndipo, Waamaleki na Wakanaani waliokaa huko mlimani walipotelemka, wakawapiga, wakawatawanya mpaka Horma. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na wana wa Isiraeli, uwaambie: Mtakapoingia katika nchi yenu ya kukaa, ninayotaka kuwapa, hapo mtakapomtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima au za kuchinjwa, kama ni za kuyalipa, mtu aliyoyaapa, au kama ni za kupenda kwa moyo tu, au kama ni za sikukuu zenu, amtengenezee Bwana mnuko wa kumpendeza, kama anatoa ng'ombe au mbuzi au kondoo, basi, huyo mwenye kumtoa na ampelekee Bwana toleo lake pamoja na kilaji cha tambiko, nacho kiwe vibaba vitatu vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na kibaba kimoja cha mafuta, tena kibaba kimoja cha mvinyo kuwa kinywaji cha tambiko, kama ni cha ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, au kama ni ya kuchinjwa, nacho kiwe hivyo cha kila mwana kondoo mmoja. lakini kama ni dume la kondoo, utengeneze kilaji chake cha tambiko kuwa vibaba sita vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na kibaba kimoja na nusu cha mafuta. Nacho kinywaji chake cha tambiko kiwe kibaba kimoja na nusu cha mvinyo; ukimtolea Bwana hivi, vitakuwa mnuko wa kumpendeza. Lakini kama utatengeneza ndama kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima au ya kuchinjwa ya kuyalipa, aliyoyaapa, au ya kumshukuru Bwana, utoe pamoja na ndama kilaji cha tambiko cha vibaba tisa vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na vibaba viwili vya mafuta. Tena utoe vibaba viwili vya mvinyo kuwa kinywaji cha tambiko; ukivichoma moto vitakuwa mnuko wa kumpendeza Bwana. Hivi uvitengenezee kila ng'ombe mmoja au kila dume moja la kondoo au kila mwana kondoo au kila mwana mbuzi. Kwa hesabu yao hao, mtakaowatengeneza, kwa hesabu iyo hiyo sharti mmtengenezee kila mmoja kilaji na kinywaji chake cha tambiko. Kila mwenyeji sharti avitengeneze vivyo hivyo akitaka kumtolea Bwana ng'ombe ya tambiko kuwa mnuko wa moto wa kumpendeza. Kama kwenu yuko mgeni au mwingine anayekaa siku zote kwao walio vizazi vyenu, naye akitaka kumtengenezea Bwana ng'ombe ya tambiko kuwa mnuko wa moto wa kumpendeza, na aitengeneze vivyo hivyo, kama ninyi mnavyoitengeneza. Maongozi yawe yayo hayo ya mkutano wote, kama ni ninyi wenyewe au kama ni mgeni akaaye ugenini kwenu; maongozi haya yawe ya kale na kale ya kuviongoza vizazi vyenu; kama ninyi mlivyo mbele ya Bwana, ndivyo, naye mgeni atakavyokuwa mbele yake. Nayo maonyo na maamuzi yawe yayo hayo ya ninyi wenyewe na ya mgeni atakayekaa ugenini kwenu. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na wana wa Isiraeli, uwaambie: Mtakapoingia katika nchi ile, mimi nitakakowaingiza, mtakapokula mikate ya nchi hiyo, sharti mmtolee Bwana vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa. Mlimbuko wa unga wenu wa chengachenga uwe andazi, mtakalolitoa kuwa kipaji cha tambiko cha kunyanyuliwa, nacho mkitoe vivyo hivyo, kama mnavyokitoa kipaji cha tambiko cha kunyanyuliwa kitokacho penye kupuria ngano. Hivyo ndivyo, mtakavyompa Bwana malimbuko ya unga wenu wa chengachenga kuwa vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa. Ikiwa kwa kupotelewa, msiyafanye hayo maagizo yote, Bwana aliyomwambia Mose, nayo hayo yote, Bwana aliyowaagiza ninyi kinywani mwa Mose tangu siku ile, Bwana alipoanza kuwaagiza maneno, nayo aliyoyaagiza baadaye kwa vizazi na vizazi, kama ni makosa yaliyofanyika kwa kupotelewa tu, ikiwa wao wa mkutano hawakuyaona, basi, mkutano wote na utengeneze dume moja la ng'ombe aliye kijana bado kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima kuwa mnuko wa kumpendeza Bwana; waitoe pamoja na kilaji na kinywaji chake cha tambiko, kama ilivyo desturi, tena watoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. Naye mtambikaji na aupatie upozi mkutano wote wa wana wa Isiraeli, waondolewe hayo makosa, kwani walipotelewa tu. Nao wenyewe na wayapeleke matoleo yao kuwa ng'ombe za tambiko za Bwana za kuteketezwa, nazo ng'ombe za tambiko za weuo wao na wamtolee Bwana usoni pake kwa ajili ya kupotelewa kwao. Hivyo ndivyo, wao wa mkutano wote wa wana wa Isiraeli pamoja na wageni watakaokaa ugenini kwao watakavyoondolewa makosa, kwa kuwa watu wote walikuwa wamepotelewa. Kama mtu mmoja anakosa kwa kupotelewa, na atoe mbuzi jike wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. Naye mtambikaji na ampatie upozi mtu huyo aliyepotelewa, akitoa mbele ya Bwana ng'ombe ya tambiko ya kumweua kwa ajili ya kupotelewa kwake; akimpatia upozi hivyo, ataondolewa kosa lake. Kama ni mwenyeji wa wana wa Isiraeli, au kama ni mgeni atakayekaa ugenini kwenu, maongozi yawe yayo hayo ya kuwafanyizia waliokosa kwa kupotelewa. Lakini mtu akikosa kwa kusudi, kama ni mwenyeji, au kama ni mgeni, huyo anamtukana Bwana, kwa hiyo mtu aliye hivyo sharti ang'olewe katikati yao walio ukoo wake, kwani amelibeza Neno la Bwana na kuyavunja maagizo yake. Mtu aliye hivyo hana budi kung'olewa kabisa na kutwikwa manza, alizozikora. Wana wa Isiraeli walipokuwa nyikani waliona mtu, akiokota kuni siku ya mapumziko. Waliomwona, alivyookota kuni, wakampeleka kwa Mose na Haroni na kwa mkutano wote. Wakamweka kifungoni, kwani haijaelekea bado, mtu kama huyu atakayofanyiziwa. Bwana akamwambia Mose: Mtu huyu hana budi kuuawa, wao wote wa mkutano na wampige mawe nje ya makambi. Ndipo, wao wote wa mkutano walipomtoa na kumpeleka nje ya makambi, wakampiga mawe, hata akafa, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Bwana akmwambia Mose kwamba: Sema na wana wa Isiraeli, uwaambie, wajifanyizie vishada penye ncha za mavazi yao, wao na vizazi vyao, kisha juu ya hivyo vishada watie nyuzi za rangi za nguo za kifalme. Maana ya hivyo vishada vyenu ni hii: mtakapoviona, myakumbuke maagizo yote ya Bwana, myafanye, msizifuate tamaa za mioyo yenu na za macho yenu, kwani mkizifuata hufanya ugoni. Kwa hiyo yakumbukeni maagizo yangu na kuyafanya, mpate kuwa watakatifu wa Mungu wenu. Mimi Bwana ni Mungu wenu aliyewatoa ninyi katika nchi ya Misri, niwe Mungu wenu; kweli mimi Bwana ni Mungu wenu. Kora, mwana wa Isihari, mwana wa Kehati, mwana wa Lawi, akachukua watu, yeye na Datani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Peleti, waliokuwa wana wa Rubeni. Hawa wakamwinukia Mose pamoja na wana wa Isiraeli 250 waliokuwa wakuu mashaurini na wateule wa mkutano wenye jina kuu. Wakakusanyika kutetana na Mose na Haroni, wakawaambia: Maneno yenu ni mengi, kwani wao wote wa mkutano wetu mzima ni watakatifu, naye Bwana yuko katikati yao. Mbona mnajikweza kuwa wakuu wao wa mkutano wa Bwana? Mose alipoyasikia akaanguka kifudifudi, akamwambia Kora nao wenzake wote, aliowakusanya, kwamba: Kesho Bwana atamjulisha aliye wake naye aliye mtakatifu akimfikisha kwake; kwani atakayemchagua atamfikisha kwake. Fanyeni haya: jichukulieni vyetezo, wewe Kora na wenzako wote, uliowakusanya! Tieni moto humo, kisha wekeni kesho mavukizo juu yao mbele ya Bwana! Naye mtu, Bwana atakayemchagua, na awe mtakatifu. Maneno yenu ni mengi, ninyi wana wa Lawi. Kisha Mose akamwambia Kora: Sikieni, ninyi wana wa Lawi! Je? Ni kidogo kwenu, Mungu wa Isiraeli akiwatenga ninyi kwao wa mkutano wa Waisiraeli na kuwafikisha kwake, mwutumikie utumishi wa Kao lake Bwana na kusimama mbele ya mkutano kwa kuutumikia? Wewe na ndugu zako wote walio wana wa Lawi amewafikisha kwake pamoja na wewe, tena mnautafutiaje utambikaji nao? Kweli wewe pamoja na wenzako wote mnafanya shauri la kumpingia Bwana, kwani Haroni ni nani, mkimnung'unikia? Kisha Mose akatuma kumwita Datani na Abiramu, wana wa Eliabu, lakini wakasema: Hatuji. Ni kidogo, ukitutoa katika nchi ichuruzikayo maziwa na asali, utuue huku nyikani? Unajikuzaje tena kuwa mkuu wa kututawala? Kweli umetuingiza katika nchi ichuruzikayo maziwa na asali! Kweli umetugawia mashamba na mizabibu kuwa yetu! Watu hawa unataka kuwachoma macho? Hatuji. Ndipo, Mose alipokasirika sana, akamwambia Bwana: Usigeuke kuvitazama vilaji vyao vya tambiko! Sikuchukua kwao hata punda mmoja tu, wala mtu wa kwao sikumfanyizia mabaya hata mmoja tu. Kisha Mose akamwambia Kora: Wewe na wenzako wote, uliowakusanya, sharti mwe kesho mbele ya Bwana, wewe nao wale na Haroni. Mchukue kila mmoja chetezo chake, mtie humo mavukizo, kisha mmtokee Bwana kila mmoja na chetezo chake, vyote viwe vyetezo 250, wewe nawe na Haroni, kila na chake chetezo. Wakachukua kila mtu chetezo chake, wakatia moto humo, juu ya moto wakaweka mavukizo, wakaja kusimama hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, hata Mose na Haroni walikuwako. Lakini Kora alikuwa aliwakusanya hao wa mkutano wote hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano; ndipo, utukufu wa Bwana ulipoutokea huo mkutano wote. Naye Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba: Jitengeni na kutoka katikati yao wa mkutano huu! Kwani nitawamaliza kwa mara moja. Wakaanguka kifudifudi, wakasema: Mungu uliye Mungu wa roho zao wote walio wenye miili, mtu mmoja akikosa, utawachafukia wote wa mkutano huu? Ndipo, Bwana alipomwambia Mose kwamba: Waambie wao wa mkutano huu kwamba: Epukeni kabisa po pote panapoyazunguka makao ya Kora na ya Datani na ya Abiramu! Kisha Mose akainuka, akaenda kwao Datani na Abiramu, nao wazee wa Waisiraeli wakamfuata. Akasema nao wa mkutano kwamba: Ondokeni penye mahema ya watu hawa wasiomcha Mungu! Wala msiguse cho chote kilicho chao, msiangamizwe kwa ajili ya makosa yao yote. Ndipo, walipoepuka po pote palipoyazunguka makao ya Kora na ya Datani na ya Abiramu, lakini Datani na Abiramu wakatoka, wakasimama hapo pa kuyaingilia mahema yao pamoja na wake zao na wana wao na watoto wao wachanga. Kisha Mose akasema: Hivi ndivyo, mtakavyotambua, kama Bwana alinituma, niyafanye hayo matendo yote, au kama ni moyo wangu ulionituma: watu hawa watakapokufa, kama watu wote wanavyokufa, au watakapopatwa na mambo, watu wote wanayopatwa nayo, Bwana hakunituma. Lakini Bwana akiumba jambo jipya, nchi ikiasama na kuwameza wao pamoja navyo vyote vilivyo vyao, washuke kuzimuni wakiwa wazima, ndipo, mtakapotambua, ya kuwa watu hao wamemtukana Bwana. Ikawa, alipokwisha kuyasema maneno haya, ndipo, nchi ilipoatuka chini yao, maana nchi ikaasama, ikawameza wao pamoja na nyumba zao, nao watu wote waliokuwa upande wa Kora, nazo mali zao zote. Ndivyo, walivyoshuka kuzimuni pamoja navyo vyote vilivyokuwa vyao wakiwa wazima, kisha nchi ikawafunika, wakawa wametoweka katikati yao wa mkutano huu. Nao Waisiraeli wote waliosimama hapo na kuwazunguka wakakimbia kwa makelele yao, kwani walisema: Nchi isitumeze na sisi! Kisha moto ukatoka kwake Bwana, ukawala wale watu 250, walipokuwa wanavukiza. Bwana akamwambia Mose kwamba: Mwambie Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, aviokote vyetezo hapo, wale walipoteketezwa, kwani ni vitakatifu; nayo makaa ya moto uyamwage huko na huko. Kisha hivyo vyetezo vya hao wakosaji waliojipatia kufa wenyewe vitengenezeni kuwa mabati mapana ya kuifunikiza meza ya kutambikia. Kwa kuwa walivitokeza mbele ya Bwana, ni vitakatifu, navyo sharti viwe kielekezo kwao wana wa Isiraeli. Naye mtambikaji Elazari akavichukua hivyo vyetezo vya shaba, wao walioteketea walivyovitokeza mbele ya Bwana, wakavisana, viwe kifuniko cha meza ya kutambikia. Hivyo vikawa ukumbusho wa wana wa Isiraeli, kwa kwamba mtu mgeni asiye wa uzao wa Haroni, asije kuvukiza mavukizo mbele ya Bwana, asipatwe na mambo kama Kora na wenzake, aliowakusanya, maana Bwana alivyomwambia kinywani mwa Mose yalimpata. Kesho yake wao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli wakamnung'unikia Mose na Haroni kwamba: Mmewaua watu wa Mungu. Ikawa, huo mkutano ulipokusanyika kutetana na Mose na Haroni, nao hao walipoligeukia Hema la Mkutano, mara lile wingu likalifunika, nao utukufu wa Bwana ukatokea. Mose na Haroni walipokwenda kufika hapo mbele ya Hema la Mkutano, Bwana akamwambia Mose kwamba: Jiepusheni katikati ya mkutano huu, niwamalize kwa mara moja! Ndipo, walipoanguka kifudifudi, naye Mose akamwambia Haroni: Chukua chetezo, utie humo moto wa mezani pa kutambikia, kisha weka mavukizo juu yake, uende upesi kwenye mkutano, uwapatie upozi, kwani makali yamekwisha kutoka kwake Bwana, nalo pigo limekwisha kuwaanzia. Haroni akachukua chetezo, kama Mose alivyosema, akapiga mbio kufika katikati ya mkutano, akaona, ya kuwa pigo limeanza kweli kupiga watu; ndipo, alipotia mavukizo juu ya moto, awapatie watu upozi. Aliposimama katikati yao waliokufa nao walio wazima bado, hilo pigo likakomeshwa. Nao waliouawa na hilo pigo walikuwa watu 14700, wasipohesabiwa waliokufa kwa ajili ya Kora. Kisha Haroni akarudi kwa Mose hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, hilo pigo lilipokuwa limekomeshwa. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na wana wa Isiraeli, uchukue kwao fimbo, kwa kila mlango wa baba fimbo moja, wao wakuu wote wa milango ya baba zao wakupe fimbo 12, nawe uandike kila fimbo jina la mwenyewe. Nalo jina la Haroni uliandike katika fimbo ya Lawi, kwani kila fimbo moja iwe ya kichwa cha mlango wa baba zao. Kisha uziweke Hemani mwa Mkutano chini mbele ya Sanduku la Ushahidi hapo, ninapokutana nanyi. Ndipo, fimbo yake yeye, niliyemchagua, itakapochipuka, niyakomeshe manung'uniko ya wana wa Isiraeli, wanayowanung'unikia ninyi, yasifike tena kwangu. Mose akayaambia wana wa Isiraeli; ndipo, wakuu wao wote walipompa fimbo, kila mtu mmoja fimbo moja ya mlango wa baba zao, zikawa fimbo 12, nayo fimbo ya Haroni ilikuwa katikati yao. Mose akaziweka hizi fimbo mbele ya Bwana Hemani mwa Ushahidi. Ikawa, Mose alipoliingia Hema la Ushahidi kesho yake, akaiona fimbo yake Haroni ya mlango wa Lawi, ilikuwa imechipuka, ikachanua maua, ikazaa malozi. Ndipo, Mose alipozitoa hizo fimbo zote mbele ya Bwana, akazipelekea wana wa Isiraeli, nao walipoziona wakachukua kila mtu fimbo yake. Kisha Bwana akamwambia Mose: Irudishe fimbo ya Haroni hapo mbele ya Sanduku la Ushahidi, iwekwe kuwa kielekezo chao hawa wana wakatavu, manung'uniko yao yakome, yasifike tena kwangu, wao wasife. Mose akavifanya; kama Bwana alivyomwagiza, ndivyo livyovifanya. Kisha wana wa Isiraeli wakamwambia Mose kwamba: Tazama, tunakufa, tunaangamia, kweli sisi sote tunaangamia. Kila alifikiaye Kao la Bwana, kweli kila alifikiaye karibu hufa; je? hivi hatutakwisha kufa sote? 4 Mose. 16:40. Bwana akamwambia Haroni: Wewe na wanao na mlango wa baba yako pamoja na wewe mtatwikwa maovu yatakayoonekana Patakatifu; tena wewe pamoja na wanao mtatwikwa maovu ya utambikaji wenu. Nao ndugu wa shina la Lawi lililo shina la baba yako uwachukue, waandamane na wewe na kukutumikia wewe pamoja na wanao, mkifanya kazi zenu mbele ya Hema la Ushahidi. Kazi zao zinazowapasa kuziangalia ni kukuangalia wewe na kuliangalia Hema lote, wasikaribie tu vyombo vya Patakatifu na meza ya kutambikia, wasife wao nao pamoja nanyi. Sharti waandamane na wewe, waziangalie kazi za Hema la Mkutano ziwapasazo kuziangalia za utumishi wote wa kulitumikia Hema, lakini mgeni asiwakaribie ninyi. Kazi zenu zinazowapasa ninyi kuziangalia ni kupaangalia Patakatifu na kuiangalia meza ya kutambikia, makali yangu yasiwatokee tena wana wa Isiraeli. Tazama, mimi nimewatoa ndugu zenu Walawi katikati yao wana wa Isiraeli, nikawapa ninyi kuwa vipaji vya Bwana kwa kuutumikia utumishi wote wa Hema la Mkutano. Nawe wewe pamoja na wanao sharti mwuangalie utambikaji wenu, mfanye kazi zote za utumishi za meza ya kutambikia nazo za Chumbani mbele ya pazia, kwani ninawapa utambikaji wenu kuwa kipaji mlichopewa, lakini mgeni atakayeukaribia hana budi kuuawa. Bwana akamwambia Haroni: Tazama, mimi nimekupa kuviangalia vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa, ninavyotolewa; kwa hiyo ninakupa vipaji vitakatifu vyote, wana wa Isiraeli wanavyovitoa, kuwa ujira wako wewe na wa wanao wa kupakwa mafuta. Hii na iwe haki yenu ya kale na kale. Vitakavyokuwa vitakatifu vyenyewe vitakuwa vyako, visichomwe moto, navyo ni hivi: matoleo yao yote, vilaji vyao vya tambiko na ng'ombe zao za tambiko za weuo nazo za upozi, watakazonitolea mimi, ni matakatifu yenyewe kuwa yako na ya wanao. Na myale mahali palipo patakatifu penyewe; wote walio wa kiume na wayale, na yawe matakatifu yako. Tena ninakupa wewe na wanao wa kiume na wa kike kuwa vyenu: vipaji vyao vya tambiko, wanavyovitoa vya kunyanyuliwa, navyo vipaji vya tambiko vya wana wa Isiraeli vya kupitishwa motoni viwe vyako; hii na iwe haki yenu ya kale na kale. Kila atakayekuwa nyumbani mwako, akiwa ametakata, na avile. Tena mafuta yote yaliyo mazuri mno nazo mvinyo mbichi zilizo nzuri mno nazo ngano, watakazomtolea Bwana za malimbuko, ninakupa wewe. Nayo mazao yote ya kwanza ya nchi yao, watakayomtolea Bwana, yatakuwa yako; kila atakayekuwa nyumbani mwako, akiwa ametakata, na ayale. Navyo vyo vyote vitakavyotiwa mwiko wa kuwa vyao Waisiraeli vitakuwa vyako. Naye kila mwana wa kwanza wa mama yake, kama ni wa mtu au wa nyama wa kufuga, atakuwa wako kwao wote walio wenye miili ya nyama, watu watakaomtolea Bwana, lakini mwana wa mtu utamtoa, akombolewe, vilevile mwana wa nyama aliye mwenye uchafu utamtoa, akombolewe. Akiwa mwenye mwezi mmoja utamtoa, akombolewe kwa hivyo, utakavyompima kiasi chake cha fedha, walipe kama fedha tano, lakini fedha hizo zinazotumika Patakatifu, fedha moja kwa thumuni nane. Lakini wana wa kwanza wa ng'ombe au wa kondoo au wa mbuzi usiwatoe kukombolewa, kwani ndio watakatifu; damu zao sharti uzinyunyizie meza ya kutambikia, nayo mafuta yao sharti uyachome moto kuwa mnuko mzuri wa moto wa kumpendeza Bwana. Lakini nyama zao zitakuwa zako, kama vidari vilivyo vipaji vya tambiko vya kupitishwa motoni au kama mapaja ya kuume yalivyo yako. Tena ninakupa vipaji vitakatifu vyote, wana wa Isiraeli watakavyomtolea Bwana kuwa vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa; hivi ninakupa wewe pamoja na wanao wa kiume na wa kike; hii na iwe haki yenu ya kale na kale. Hili sharti liwe agano la kale na kale lisilochujuka kama chumvi, nalo umewekewa wewe pamoja na wanao mbele ya Bwana. Kisha Bwana akamwambia Haroni: Katika nchi yao wewe hutapata fungu la nchi litakalokuwa fungu lako katikati yao; mimi ni fungu lako, utakalolipata kuwa lako katikati ya wana wa Isiraeli. Tena tazama: Wana wa Lawi ninawapa mafungu ya kumi yote yatakayotolewa nao Waisiraeli kuwa fungu lao, ni ujira wa utumishi wao wa kufanya kazi za utumishi wa Hema la Mkutano. Lakini tangu sasa wana wa Isiraeli wasilifikie tena Hema la Mkutano karibu, wasijikoseshe, wakajipatia kufa. Ila Walawi tu na wazifanye kazi za utumishi wa Hema la Mkutano, nao ndio watakaotwikwa manza, watakazozikora. Haya sharti yawe maongozi ya kale na kale ya kuviongoza vizazi vyenu, nanyi hamtapata fungu la nchi kuwa lenu katikati ya wana wa Isiraeli. Kwani ninawapa Walawi mafungu ya kumi, wana wa Isiraeli watakayoyatoa kuwa vipaji vya tambiko vya kumnyanyulia Bwana; haya ninawapa Walawi kuwa fungu lao, kwa hiyo ninawaambia: Hamtapata fungu la nchi kuwa lenu katikati ya wana wa Isiraeli. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema nao Walawi, uwaambie: Mtakapoyachukua mafungu ya kumi kwao wana wa Isiraeli, niliyowapa ninyi kuwa fungu lenu kwao, nanyi sharti mtoe humo vipaji vya tambiko vya kumnyanyulia Bwana, navyo sharti viwe fungu la kumi la hayo mafungu ya kumi. Navyo hivyo vpaji vyenu vya tambiko vitawaziwa kuwa ngano zenu za mapurio yenu au mafuriko ya makamulio yenu. Nanyi mtakapovitoa hivyo vipaji vya tambiko vya kumnyanyulia Bwana vya mafungu yenu ya kumi, mtakayoyachukua kwa wana wa Isiraeli, sharti m mpe mtambikaji Haroni hivyo vipaji vya tambiko, mtakavyovitoa kwenu vya kumnyanyulia Bwana. Katika vipaji vyote, mtakavyopewa, sharti mtoe vipaji vya tambiko vyote viwapasavyo kuvitoa vya kumnyanyulia Bwana, nanyi sharti mtoe vile vitakavyokuwa vizuri zaidi vinavyopasa kutolewa humo kuwa vipaji vitakatifu. Kwa hiyo uwaambie: Mtakapotoa humo vilivyo vizuri zaidi kuwa vipaji vyenu vya tambiko vya kunyanyuliwa, vitawaziwa kuwa mapato ya Walawi ya mapurio yao na mapato ya makamulio yao. Nanyi na mvile mahali po pote ninyi nao walio wa milango yenu, kwani ni mishahara yenu ya utumishi wenu wa Hema la Mkutano. Mtakapovitoa vilivyo vizuri zaidi katika mapato yenu kuwa vipaji vya tambiko, basi, hamtajikosesha kwa ajili yao, wala hamtavichafua vipaji vitakatifu vya wana wa Isiraeli, msife. Bwana akawambia Mose na Haroni kwamba: Haya ndiyo maongozi ya mafunzo, Bwana aliyoyaagiza kwamba: Waambie wana wa Isiraeli, wakupatie ng'ombe mwekundu jike asiye na kilema wala doadoa lo lote, asiyefungwa bado kuvuta gari. Kisha mpe mtambikaji Elazari, ampeleke kufika nje ya makambi, ndipo wamchinje machoni pake. Kisha mtambikaji Elazari achukue kwa kidole chake damu yake kidogo, ainyunyizie mara saba hapo panapolielekea Hema la Mkutano. Kisha wamteketeze machoni pake, nao sharti wateketeze ngozi yake na nyama zake na damu yake pamoja na mavi yake. Naye mtambikaji na achukue kipande cha mwangati na kivumbasi na nyuzi nyekundu, azitupe katika huo moto unaomteketeza huyo ng'ombe. Kisha mtambikaji na azifue nguo zake pamoja na kuuogesha mwili wake majini, kisha aingie makambini, lakini atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye aliyemteketeza sharti azifue nguo zake majini na kuuogesha mwili wake majini, lakini naye atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Kisha mtu mwenye kutakata na ayazoe majivu yake huyo ng'ombe, ayaweke nje ya makambi mahali palipo penye kutakata, yakae hapo hapo na kuangaliwa, yawe tayari, mkutano wa wana wa Isiraeli watakapoyatumia ya kutengeneza maji ya kunyunyiza, kwani ni ng'ombe ya tambiko ya weuo. Naye aliyeyazoa hayo majivu ya huyo ng'ombe sharti azifue nguo zake, lakini atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Haya yawe maongozi ya kale na kale kwa wana wa Isiraeli na kwa wageni watakaokaa ugenini katikati yao. Atakayegusa mfu wa mtu ye yote atakuwa mwenye uchafu siku saba. Naye ajieue kwa yale maji ya kunyunyiza siku ya tatu, ndipo, atakapokuwa siku ya saba mwenye kutakata; lakini asipojieua siku ya tatu wala siku ya saba hatakuwa mwenye kutakata. Kila mtu atakayegusa mfu, ni kwamba maiti ya mtu ye yote aliyekufa, asipojieua hulichafua Kao la Bwana; mtu aliye hivyo sharti ang'olewe kwao Waisiraeli. Kwa kuwa hakunyunyiziwa hayo maji ya kunyunyiza, ni mwenye uchafu, nao huo uchafu wake utamkalia vivyo hivyo. Nayo haya maonyo sharti yaangaliwe, mtu akifa hemani: kila atakayeingia humo hemani naye kila atakayekuwamo humo hemani atakuwa mwenye uchafu siku saba. Nacho kila chombo kilicho wazi kisichofunikwa na kifuniko cha kukifungia kabisa ni chenye uchafu. Hata kila mtu atakayegusa porini mtu aliyeuawa kwa upanga au mfu au mfupa wa mtu au kaburi atakuwa mwenye uchafu siku saba. Mtu akiwa mwenye uchafu hivyo, na wachukue majivu machache ya hiyo ng'ombe ya weuo iliyoteketezwa, wayatie chomboni, kisha watie humo maji ya mtoni. Kisha mtu mwenye kutakata na achukue kivumbasi, akichovye katika hayo maji, ayanyunyizie lile hema na vyombo vyote vilivyomo nao watu wote waliokuwamo naye yule mtu aliyegusa mfupa wa mzoga wa mtu aliyeuawa kwa upanga au mfu au kaburi. Ndivyo, mwenye kutakata atakavyomnyunyizia mwenye uchafu siku ya tatu na siku ya saba; akiisha kumweua hiyo siku ya saba sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, ndivyo, atakavyokuwa jioni mwenye kutakata. Lakini mtu akiwa mwenye uchafu pasipo kujieua, basi, aliye hivyo hana budi kung'olewa katika mkutano huu, kwani hupachafua Patakatifu pa Bwana, kwani asiponyunyiziwa hayo maji ya kunyunyiza, ni mwenye uchafu vivyo hivyo. Haya yawe kwao maongozi ya kale na kale. Naye yule aliyemnyunyizia mwenzake hayo maji ya kunyunyiza sharti azifue nguo zake. Naye atakayeyagusa hayo maji ya kunyunyiza atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Navyo vyote, mwenye uchafu atakavyovigusa, vitakuwa vyenye uchafu, naye kila mtu, atakayemgusa, atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Mkutano wote wa wana wa Isiraeli walipofika katika nyika ya Sini katika mwezi wa kwanza, watu wakakaa Kadesi. Ndiko, Miriamu alikokufa; kisha akazikwa huko. Wao wa mkutano wasipoona maji huko, wakamkusanyikia Mose na Haroni, wakamgombeza Mose wakimwambia kwamba: Afadhali tungalizimia roho pamoja na ndugu zetu waliozimia roho mbele ya Bwana! Kwa nini mmelileta kundi lake Bwana katika nyika hii, tujifie pamoja na nyama wetu wa kufuga? Kwa nini mlitutoa Misri, mkatuleta mahali hapa pabaya? Huku hatuwezi kupanda mbegu, tena hakuna mikuyu wala mizabibu wala mikomamanga, wala maji tu ya kunywa hayako huku. Mose na Haroni wakatoka hapo, walipokusanyika, wakaenda hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano; napo hapo, walipoanguka kifudifudi, utukufu wa Bwana ukawatokea. Bwana akamwambia Mose kwamba: Ichukue ile fimbo! Kisha wewe na kaka yako Haroni wakusanyeni wao wote wa mkutano, mseme na mwamba huu machoni pao wote, ndipo, utakapowapa maji yake. Ndivyo, utakavyowatolea maji humu mwambani, uwanyweshe wao wa mkutano pamoja na nyama wao wa kufuga. Mose akaichukua fimbo iliyokuwa mbele ya Bwana, kama Bwana alivyomwagiza. Kisha Mose na Haroni wakalikusanya kundi la watu mbele ya mwamba, akawaambia: Sikieni, ninyi msiotii! Itakuwaje? Tutaweza kuwatolea ninyi maji humu mwambani? Kisha Mose akauinua mkono wake, akaupiga mwamba kwa fimbo yake mara mbili; ndipo, maji yalipotoka mengi, wao wa mkutano wakanywa wenyewe nao nyama wao wa kufuga. lakini Bwana akamwambia Mose naye Haroni: Kwa kuwa hamkunitegemea na kunitakasa machoni pao wana wa Isiraeli, kwa hiyo hamtaliingiza kundi hili katika ile nchi, nitakayowapa. Maji yale yakaitwa Meriba (Magomvi), kwa kuwa wana wa Isiraeli waligombana na Bwana, naye akajitokeza kwao kuwa mtakatifu. Kule Kadesi Mose akatuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu kwamba: Hivi ndivyo, ndugu yako Isiraeli anavyosema: Wewe unayajua masumbuko yote yaliyotupata: baba zetu walishuka Misri, wakakaa huko siku nyingi, nao Wamisri wakatufanyizia mabaya sisi na baba zetu. Tulipomlilia Bwana, akatusikia, akatuma malaika, akatutoa Misri. Tazama, sisi tumo humo Kadesi, ndio mji wa mpakani kwenye nchi yako. Sasa tunataka kupita katika nchi yako, lakini hatutaki kupita mashambani wala mizabibuni, wala hatutakunywa maji ya visimani, ila tunataka kuishika njia ya mfalme tu, tusiiache kwenda kuumeni wala kushotoni, hata tuupite mpaka wako mwingine. Lakini Mwedomu akamwambia: Hutapita kwangu. Ila nitatoka mwenye upanga, nipigane na wewe. Wana wa Isiraeli wakamwambia: Tunataka kushika njia tu, tena tukinywa maji yako sisi na nyama wetu wa kufuga tutakulipa; hakuna jingine, tunalolitaka, ila kupita tu kwa miguu yetu. Lakini akasema: Huna ruhusa kupita. Kisha Waedomu wakatoka wenye watu wengi na wenye mikono ya nguvu, wawazuie. Ndivyo, Waedomu walivyowakataza Waisiraeli kupita mipakani kwao; ndipo, Waisiraeli walipogeuka, washike njia ya kupitia kando yao. Kisha wana wa Isiraeli wakaondoka Kadesi, wakafika mkutano wao wote kwenye mlima wa Hori. Huko kwenye mlima wa Hori kwenye mipaka ya nchi ya Edomu Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba: Sasa Haroni atachukuliwa, awe pamoja nao walio wa ukoo wake, kwani hataingia katika nchi ile, nitakayowapa wana wa Isiraeli, kwa kuwa mlikibishia kinywa changu kwenye Maji ya Magomvi. Mchukue Haroni pamoja na mwanawe Elazari, uwapeleke mlimani kwa Hori juu. Huko umvue Haroni mavazi yake, umvike mwanawe Elazari! Kisha Haroni atachukuliwa, afe huko. Mose akafanya, kama Bwana alivyomwagiza, wakaupanda mlima wa Hori machoni pao wote walio wa mkutano. Kisha Mose akamvua Haroni mavazi yake, akamvika mwanawe Elazari; ndipo, Haroni alipokufa huko juu mlimani, kisha Mose na Elazari wakashuka mlimani. Wote wa mkutano walipoona, ya kuwa Haroni amekwisha kufa, wakamwombolezea Haroni siku thelathini wao wote wa mlango wa Isiraeli. Mfalme wa Kikanaani wa Aradi aliyekaa upande wa kusini aliposikia, ya kuwa Waisiraeli wanakuja wakiifuata njia ya wapelelezi, akapigana nao Waisiraeli, akateka wengine wa kwao. Ndipo, Waisiraeli walipomwapia Bwana kiapo cha kwamba: Ukiwatia watu hawa mikononi mwetu, tutaiangamiza miji yao kwa kuitia mwiko wa kuwapo. Bwana akazisikia sauti zao Waisiraeli, akawapa hao Wakanaani, nao wakawaangamiza wao pamoja na miji yao kwa kuitia mwiko wa kuwapo; kwa hiyo wakapaita mahali pale Horma (Mwiko). Kisha wakaondoka kwenye mlima wa Hori wakishika njia ya kwenda kwenye Bahari Nyekundu, waizunguke nchi ya Edomu. Watu walipotaka kuzimia roho kwa kuchoka njiani, wakamgombeza Mungu, hata Mose kwamba: Kwa nini mlitutoa Misri, tujifie huku nyikani? Kwani hakuna chakula wala maji, nazo roho zetu zinachukizwa na chakula hiki kikosacho nguvu. Ndipo, Bwana alipotuma nyoka za moto kuwajia hao watu; nao walipowauma watu, wakafa watu wengi kwao Waisiraeli. Ndipo, watu walipomjia Mose, wakasema: Tumekosa tulipomgombeza Bwana, hata wewe. Tuombee kwake Bwana, awaondoe hawa nyoka kwetu! Mose alipowaombea hao watu, Bwana akamwambia Mose: Jitengenezee nyoka ya moto, uitungike kuwa kielekezo! Itakuwa, kila aliyeumwa na nyoka atakapoitazama atapona. Mose akatengeneza nyoka ya shaba nyekundu, akaitungika kuwa kielekezo, ikawa hivyo: nyoka alipomwuma mtu, naye akaitazama hiyo nyoka ya shaba, akapona. Waisiraeli walipoondoka huko, wakapiga makambi Oboti. Walipoondoka Oboti wakapiga makambi Iye-Abarimu katika nyika inayoelekea Moabu upande wa maawioni kwa jua. Walipoondoka huko, wakapiga makambi kwenye kijito cha Zeredi. Walipoondoka huko, wakapiga makambi kwenye kijito cha Zeredi. Walipoondoka huko wakapiga makambi ng'ambo ya huko ya Arnoni ulioko nyikani, utokao mipakani kwa Waamori, kwani Arnoni ulikuwa mpaka wa Wamoabu kuwatenga Wamoabu na Waamori. Kwa hiyo inasemwa katika kitabu cha vita vya Bwana: Bonde la Sufa na vijito vya Arnoni, napo vijito vinaposhukia, panapopafikia napo mahali penye mji wa Ari ndipo panapouegemea mpaka wa Moabu. Toka hapo wkafika Kisimani; ndiko kwenye kile kisima, Bwana alikomwambia Mose kwamba: Wakusanye watu, niwape maji! siku zile Waisiraeli waliuimba wimbo huu: Bubujika, kisima! Haya! Kiimbieni! Waliokichimba kisima hiki ndio wakuu; kweli majumbe wa watu ndio waliokifukua. kwa kutumia bakora na fimbo zao za kifalme. Toka huko nyikani wakaenda Matana. Toka Matana wakaenda Nahalieli, toka Nahalieli wakaenda Bamoti, toka Bamoti wakaenda bondeni kwenye mbuga za Moabu zilizoko kwenye mlima na Pisiga uelekeao jangwani. Waisiraeli wakatuma wajumbe kwa Sihoni, mfalme wa Waamori, kwamba: Tunataka kupita katika nchi yako; hatutaondoka njiani kuingia mashambani au mizabibuni, wala hatutakunywa maji ya visimani, ila tunataka kuishika njia ya mfalme tu, hata tuupite mpaka wako mwingine. Lakini Sihoni hakuwapa wana wa Isiraeli ruhusa kupita mipakani kwake, ila Sihoni akawakusanya watu wake wote, akatoka kwenda nyikani kuwazuia Waisiraeli. Alipofika Yasa akapigana nao Waisiraeli. lakini Waisiraeli wakampiga kwa ukali wa panga, wakaichukua nchi yake toka mto wa Arnoni mpaka mto wa Yakobo, wana wa Amoni walikokaa, kwani mipaka yao wana wa Amoni ilikuwa yenye nguvu. Waisiraeli wakaiteka hiyo miji yote, kisha Waisiraeli wakakaa katika miji yote ya Waamori, namo Hesiboni na katika mitaa yake yote. Kwani Hesiboni ulikuwa mji wa Sihoni, mfalme wa Waamori; naye aliupigania kale na mfalme wa Moabu, ndipo, alipoichukua hiyo nchi yake na kuitoa mkononi mwake mpaka mto wa Arnoni. Kwa hiyo wenye kutunga mafumbo walisema: Njoni Hesiboni, mji wa Sihoni ujengwe na kutiwa nguvu! Kwani moto umetoka Hesiboni, miali ya moto imetoka mjini mwa Sihoni, ikaula mji wa Ari wa Moabu nao wenyeji wa vilimani kwa Arnoni. Umepatwa na mambo, wewe Moabu! Mmeangamia ninyi, watu wa Kemosi! Wamewakimbiza wana wenu wa kiume, nao wana wenu wa kike wamempa Sihoni, mfalme wa Waamori! Tulipowapiga mishale, ndipo, Hesiboni ulipoangamia mpaka Diboni, tukaiharibu nchi mpaka Nofa, tukafika hata Medeba. ndipo, Waisiraeli walipokaa katika nchi ya Waamori. Kisha Mose akatuma watu kwenda Yazeri kupeleleza, nao wakaiteka mitaa yake na kuwafukuza Waamori waliokuwamo. Kisha wakageuka, wakaishika njia ya kupanda Basani. Lakini Ogi, mfalme wa Basani, akatoka kuwazuia, yeye na watu wake wote, wakapigana huko Edirei. Bwana akamwambia Mose: Usimwogope, kwani nimemtia mkononi mwako pamoja na watu wake wote, hata nchi yake, umfanyizie, kama ulivyomfanyizia Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekaa Hesiboni. ndipo, walipompiga yeye na wanawe na watu wake wote, wasisaze kwake hata mmoja aliyeweza kukimbia, kisha wakaitwaa nchi yake. Wana wa Isiraeli walipoondoka huko wakapiga makambi kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili. Balaka, mwana wa Sipori, alipoyaona yote, Waisiraeli waliyowafanyizia Waamori, Wamoabu wakaingiwa na woga mwingi sana wa hao watu kwa kuwa wengi sana, nao Wamoabu wakawastukia sana wana wa Isiraeli. Ndipo, Wamoabu walipowaambia wazee wa Wamidiani: Makundi hayo yatameza yote yanayotuzunguka, kama ng'ombe anavyomeza majani ya porini. Ndipo, Balaka, mwana wa Sipori, aliyekuwa mfalme wa Wamoabu siku zile alipotuma wajumbe kwenda Petori kwa Bileamu, mwana wa Beori, aliyekaa kwenye lile jito kubwa katika nchi yao walio ukoo wake, wamwite na kumwambia: Tazama, wako watu waliotoka Misri, nao wanaifunika nchi hii pote, unapotazama, tena wanakaa kunielekea mimi. Sasa njoo, uniapizie watu hawa! Kwani wako na nguvu za kunishinda mimi. Hivyo labda nitaweza kuwapiga na kuwafukuza katika nchi hii, kwani ninajua: Utakayembariki atakuwa amebarikiwa, naye utakayemwapiza atakuwa ameapizwa. Ndipo, wazee wa Wamoabu na wazee wa Wamidiani walipokwenda wakiushika mshahara wa uaguaji mikononi mwao; nao walipofika kwa Bileamu wakamwambia maneno ya Balaka. Akawaambia: Laleni huku usiku huu! Nami na niwarudishie neno, kama Bwana atakavyoniambia. Kwa hiyo wale wakuu wa Wamoabu wakakaa kwake Bileamu. Mungu akaja kwake Bileamu, akamwuliza: Watu hawa wanaokaa kwako ni watu gani? Bileamu akamwambia Mungu: Balaka, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu kwamba: Tazama, wako watu waliotoka Misri, nao wanaifunika nchi pote, unapotazama; sasa njoo, uniapizie watu hawa! Labda hivyo nitaweza kupigana nao na kuwafukuza. Lakini Mungu akamwambia Bileamu: Usiende nao! Wala usiwaapize watu hao, kwani wamebarikiwa. Bileamu alipoamka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaka: Nendeni zenu katika nchi yenu, kwani Bwana amekataa kunipa ruhusa kwenda nanyi. Ndipo, wakuu wa Wamoabu walipoondoka; walipofika kwa Balaka wakamwambia: Bileamu amekataa kwenda na sisi. Ndipo, Balaka alipotuma tena wakuu wengi wenye utukufu zaidi kuliko wale wa kwanza. Walipofika kwa Bileamu wakamwambia: Hivi ndivyo, anavyosema Balaka, mwana wa Sipori: Usikatae kuja kwangu! Kwani nitakuheshimu sanasana, nayo yote, utakayoniambia, nitayafanya; njoo tu, uniapizie hawa watu! Bileamu akajibu, akawaambia watumishi wa Balaka: Ijapo Balaka anipe nyumba yake ijaayo fedha na dhahabu, sitaweza kukipita kinywa cha Bwana Mungu wangu, nifanye jambo dogo au kubwa. Sasa nanyi kaeni hapa usiku huu, nijue, Bwana atakayoniambia tena! Mungu akaja kwake Bileamu na usiku, akamwambia: Kama hawa watu wamekuja kukuita, inuka, uende nao! Lakini sharti ulifanye neno, nitakalokuambia. Bileamu alipoondoka asubuhi akamtandika punda wake, akaenda nao wakuu wa Moabu. Makali ya Mungu ayakawaka moto, kwa kuwa amekwenda; kwa hiyo malaika wa Bwana akaja, akajisimamisha njiani, ampinge; naye alikuwa amempanda punda wake, nao vijana wake wawili walikuwa naye. Punda alipomwona malaika wa Bwana, akisimama njiani na kushika mkononi upanga uliochomolewa, punda akaondoka njiani na kuingia porini, naye Bileamu akampiga punda, amrudishe njiani. Kisha malaika wa Bwana akasimama tena njiani penye mizabibu palipokuwa pembamba, kwa kuwa pande zote mbili palikuwa na kuta za mawe. Punda alipomwona malaika wa Bwana akajisonga ukutani na kuuchubua mguu wa Bileamu; ndipo, alipompiga tena. Naye malaika wa Bwana akapita tena, akaenda kusimama mahali pafinyu sana pasipowezekana kupitia wala kuumeni wala kushotoni. Punda alipomwona malaika wa Bwana akalala chini, naye Bileamu alikuwa juu yake. Ndipo, makali ya Bileamu yalipomwakia, akampiga punda kwa fimbo. Ndipo, Bwana alipokifumbua kinywa cha punda, akamwambia Bileamu: Nimekukosea nini, ukinipiga sasa mara ya tatu? Bileamu akamwambia punda: Kumbe unanifyoza! Kama ningekuwa na upanga mkononi mwangu, ningekuua sasa hivi. Naye punda akamwambia Bileamu: Je? Mimi si punda wako, uliyempanda siku zote za maisha yako hata siku hii ya leo? Nimezoa kukufanyizia hivyo? Akasema: La! Ndipo, Bwana alipoyafumbua macho yake Bileamu, akamwona malaika wa Bwana, alivyosimama njiani na kushika mkononi upanga uliochomolewa; ndipo, alipomwinamia na kumwangukia kifudifudi. Naye malaika wa Bwana akamwambia: Kwa nini umempiga punda wako sasa mara ya tatu? Tazama, mimi nimetoka, nikupinge. Kwani safari hii ni ya kuangamiza machoni pangu. Punda aliponiona akaondoka njiani mbele yangu sasa mara ya tatu; kama asingaliondoka njiani mbele yangu, ningalikwisha kukuua wewe mwenyewe na kumponya yeye. Ndipo, Bileamu alipomwambia malaika wa Bwana: Nimekosa, kwani sikujua, ya kuwa wewe umesimama njiani, unipinge; sasa kama safari hii ni mbaya machoni pako, nitarudi. Naye malaika wa Bwana akamwambia Bileamu: Jiendee pamoja na watu hawa! Lakini sharti uliseme neno hilo tu, nitakalokuambia. Kisha Bileamu akaenda na wale wakuu wa Balaka. Balaka aliposikia, ya kama Bileamu anakuja, akatoka kumwendea njiani mpaka kwenye mji wa Moabu ulioko mahali penye mto wa Arnoni ulioko kwenye mapeo ya mpaka. Balaka akamwuliza Bileamu: Sikutuma kwako vizuri, nikuite? Mbona hukuja kwangu? Labda unaniwazia kuwa mtu asiyeweza kukupa macheo? Naye Bileamu akamwambia Balaka: Tazama, nimefika kwako! Lakini sasa je? nitaweza kusema lo lote? Neno hilo tu, Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo, nitakalolisema. Kisha Bileamu akaenda na Balaka, wakaingia Kiriati-Husoti (Mji wenye Mabarabara). Balaka akachinja ng'ombe na kondoo kuwa ng'ombe za tambiko, akamgawia hata Bileamu nyama, hata wakuu waliokuwa naye. Ilipokuwa asubuhi, Balaka akamchukua Bileamu, akampeleka juu vilimani kwa Baali; huko ndiko, alikowaona watu hao hata mwisho wa makambi yao. Bileamu akamwambia Balaka: Nijengee hapa mahali saba pa kutambikia, kisha nipate hapa madume saba ya ng'ombe na madume saba ya kondoo. Balaka akafanya, kama Bileamu alivyosema, kisha Balaka na Bileamu wakatoa kila mahali pa kutambikia ng'ombe mmoja na kondoo mmoja. Naye Bileamu akamwambia Balaka: Simama penye ng'ombe yako ya tambiko! Lakini mimi nitakwenda, labda Bwana atakuja kunikuta; ndipo, nitakapokuambia hilo neno, atakalonionyesha. Kisha akaenda kilimani palipo peupe. Mungu alipokuja kweli kukutana na Bileamu njiani, huyu akamwambia: Nimetengeneza mahali saba pa kutambikia, nikatoa ng'ombe mmoja na kondoo mmoja kila mahali pamoja pa kutambikia. Naye Bwana akampa Bileamu maneno ya kuyasema kwa kinywa chake, kisha akamwambia: Rudi kwa Balaka, uyaseme maneno yayo hayo! Aliporudi kwake akamwona, akisimama penye ng'ombe yake ya tambiko, yeye na wakuu wote wa Moabu. Ndipo, alipoanza kusema maneno yake kwamba: Huko Aramu ndiko, alikonichukua Balaka; mfalme wa Moabu amenitoa milimani upande wa maawioni kwa jua akisema: Njoo, uniapizie Yakobo! Njoo, umchafukie Isiraeli! Lakini, Mungu asiyemwapiza nitamwapizaje? Bwana asiyemchafukia nitamchafukiaje? Hapa juu miambani ninawaona, hapa vilimani ninawachungulia; ndio watu wakaao peke yao, hawajiwazii kuwa sawa na wamizimu. Yuko nani awezaye kuyahesabu mavumbi yake Yakobo au kujua tu hesabu ya fungu la nne la Isiraeli? Kama hawa wanyofu wanavyokufa, ningetaka kufa hivyo, ningependa, mwisho wangu uwe kama mwisho wao. Ndipo, Balaka alipomwambia Bileamu: Umenifanyizia nini? Nimekuchukua, uwaapize adui zangu, kumbe umewabariki! Akajibu kwamba: Hainipasi kuangalia, niyaseme yaleyale, Bwana aliyoyatia kinywani mwangu? Ndipo, Balaka alipomwambia: Nenda pamoja na mimi mahali pengine, utakapowaona wote; sasa unaona mwisho wao tu, huwaoni wote; hapo ndipo, utakaponiapizia watu hawa. Kisha akamchukua, akampeleka juu mlimani kwa Pisiga kulikokuwa uwanda wa wachunguliaji. Huko nako akajenga mahali saba pa kutambikia, kisha akatoa kila mahali pa kutambikia ng'ombe mmoja na kondoo mmoja. Kisha Bileamu akamwambia Balaka: Simama hapa penye ng'ombe yako ya tambiko! Lakini mimi nitakwenda huko kumkuta Bwana. Naye Bwana akaja kweli kumkuta Bileamu, akampa maneno ya kuyasema kwa kinywa chake, kisha akamwambia: Rudi kwa Balaka, uyaseme maneno yayo hayo! Aliporudi kwake akamwona, akisimama penye ng'ombe yake ya tambiko pamoja na wakuu wote wa Moabu. Balaka alipomwuliza: Bwana amesema nini? akaanza kusema maneno yake kwamba: Inuka, Balaka, usikie! Nitegee sikio lako, mwana wa Sipori! Mungu si mtu, aseme uwongo, si mwana wa mtu, ageuze moyo. Yeye aseme neno, asilifanye? Aweke agano, asilitimize? Tazameni! Nimepewa kubariki; napo, alipobariki, siwezi kuyageuza. Hakuna aliyepata kutazama mambo yaliyo ya bure kwake Yakobo, wala hakuna aliyeona masumbuko kwake Isiraeli; Bwana Mungu wake yuko pamoja naye, nayo mashangilio ya mfalme husikilika kwao. Mungu ndiye aliyewatoa Misri, naye anazo nguvu kama za nyati. Kweli hakuna uganga wa kumwangamiza Yakobo, wala hakuna uaguaji wa kumponza Isiraeli, siku zote Yakobo na Isiraeli huambiwa, Mungu anayoyafanya. Na mwone, watu hawa wakiinuka kama simba mke, wakijisimamisha kama simba mume! Halali, mpaka ale nyama zao, aliowararua, mpaka anywe damu zao, aliowaua. Ndipo, Balaka alipomwambia Bileamu: Usipoweza kuwaapiza, uache kuwabariki! Lakini Bileamu akamjibu Balaka kwamba: Sikukuambia kwamba: Yote, Bwana atakayoyasema, nitayafanya? Ndipo, Balaka alipomwambia Bileamu: Njoo, nikupeleke mahali pengine, labda huko utanyoka machoni pake Mungu, ukiniapizia huko watu hawa. Kisha Balaka akamchukua Bileamu, akampeleka juu mlimani kwa Peori kunakoelekea jangwani. Huko Bileamu akamwambia Balaka: Nijengee hapa mahali saba pa kutambikia! Kisha unipatie hapa madume saba ya ng'ombe na madume saba ya kondoo. Balaka akafanya, kama Bileamu alivyosema, akatoa kila mahali pa kutambikia ng'ombe mmoja na kondoo mmoja. Bileamu alipoona, ya kuwa imekuwa vema machoni pa Bwana kuwabariki Waisiraeli, hakwenda tena kama mara ya kwanza na mara ya pili kutafuta mambo ya kuagulia, ila akauelekeza uso wake jangwani. Bileamu alipoyainua huko macho yake akawaona Waisiraeli, walivyokaa shina kwa shina; ndipo, roho ya Mungu ilipomjia, akaanza kusema maneno yake kwamba: Hivi ndivyo, asemavyo Bileamu, mwana wa Peori, hivi ndivyo, asemavyo mtu aliyefumbwa macho. Hivi ndivyo, asemavyo aliyesikia maneno ya Mungu, aliyeona maono yake aliye Mwenyezi, aliyefumbuliwa macho alipomwangukia: Mahema yako, Yakobo, ni mema peke yao, nayo makao yako, wewe Isiraeli. Huwa kama mabonde yanayoendelea mbali, huwa kama mashamba yaliyoko kando ya mto, huwa kama misagawi, Bwana aliyoipanda, huwa kama miangati iliyoko kwenye maji! Ndoo zake huchuruzisha maji mengi, nazo mbegu zake hunyweshwa maji mengi. Mfalme wake ni mkuu kuliko Agagi, nao ufalme wake utatukuka sana. Mungu ndiye aliyemtoa Misri, naye anazo nguvu kama za nyati, hula wamizimu wanaomsonga, nayo mifupa yao huipondaponda, akiwaangusha chini kwa mishale yake. Kama simba mume au simba mke anavyootea, ndivyo, anavyolala; yuko nani atakayemwinua? Mwenye kukubariki amekwisha kubarikiwa naye, mwenye kukuapiza amekwisha kuapizwa naye. Ndipo, makali ya Balaka yalipomwakia Bileamu, akayapiga makofi yake, kisha Balaka akamwambia Bileamu: Nimekuita, uwaapize adui zangu, kumbe umewabariki sasa mara ya tatu! Sasa jiendee upesi mahali pako! Nalisema moyoni: Nitakuheshimu sana, lakini tazama, Bwana amekunyima hizo heshima. Naye Bileamu akamwambia Balaka: Je? Wajumbe wako, uliowatuma kwangu, sikuwaambia kwamba: Ijapo Balaka anipe nyumba yake ijaayo fedha na dhahabu, sitaweza kukipita kinywa cha Bwana, nifanye jambo baya au jema, kama moyo wangu unavyotaka; ila Bwana atakaloniambia, ndilo hilo, nitakalolisema? Sasa tazama, ninakwenda zangu kwa watu wa kwetu; lakini kwanza nitakuonyesha, watu wa ukoo huu watakavyowafanyizia watu wako siku zitakazokuja baadaye. Kisha akaanza kusema maneno yake kwamba: Hivi ndivyo, asemavyo Bileamu, mwana wa Peori, hivi ndivyo, asemavyo mtu aliyefumbwa macho. Hivi ndivyo, asemavyo aliyesikia maneno ya Mungu, ajuaye kumtambua Alioko huko juu, aliyeona maono yake aliye Mwenyezi, aliyefumbuliwa macho alipomwangukia: Ninamtazamia, lakini hayuko sasa, ninamchungulia, lakini hayuko karibu. Nyota itatokea kwake Yakobo, nayo bakora ya kifalme itainuka kwake Isiraeli, izivunje pande zote mbili zao Wamoabu na kuwamaliza wana wao wote wapigao vita. Nayo nchi ya Edomu itakuwa yake yeye, nayo ya Seiri itakuwa yake yeye, nayo ndiyo iliyokuwa yao adui zake! Kweli Isiraeli atatenda nguvu. Mwenye kutawala atatoka mwake Yakobo, nao waliokimbia na kutoka mijini atawaangamiza. Alipowaona Waamaleki akaanza kusema maneno yake kwamba: Walio wa kwanza wa wamizimu ndio Waamaleki, lakini mwisho wao utakuwa kuangamia tu. Alipowaona Wakeni akaanza kusema maneno yake kwamba: Kao lako limeshupaa, tundu lako umelijenga mwambani, lakini havikuponyi, Kaini, utateketea, bado kidogo Waasuri watakuteka. Kisha akasema maneno yake mengine kwamba: Hoi! Yuko nani atakayepona, yatakapowapata? Nayo yatawapata hapo, Mungu atakapoyatimiza. Merikebu zitatoka kwao Wakiti, ziwanyenyekeze Waasuri, ziwanyenyekeze hata Waeberi, mpaka waangamie nao. Kisha Bileamu akaondoka kwenda kurudi kwao, naye Balaka akaenda zake. Waisiraeli walipokaa Sitimu, watu wakaanza kufanya ugoni na wanawake wa Kimoabu. Nao walipowaalikia matambiko ya miungu yao, nao hao watu wakala nyama za tambiko, hata miungu yao wakaiangukia. Lakini Waisiraeli walipojiunganisha hivyo na Baali-Peori, ndipo, makali ya Bwana yalipowawakia Waisiraeli. Kwa hiyo Bwana akamwambia Mose: Wachukue wakuu wote wa watu hawa, uwanyonge juani mbele ya Bwana, haya makali ya Bwana yawakayo moto yapate kupoa na kuwaondokea Waisiraeli. Naye Mose akawaambia waamuzi wa Waisiraeli: Waueni kila mtu watu wake waliojiunganisha na Baali-Peori! Papo hapo akaja mmoja wao wana wa Isiraeli, akapeleka kwa ndugu zake mwanamke wa Kimidiani machoni pake Mose napo machoni pao mkutano wote wa wana wa Isiraeli, hawa walipokuwa wakilia hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano. Pinehasi, mwana wa Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, alipoyaona akaondoka katikati ya mkutano, akachukua mkuki mkononi mwake, akamfuata yule mtu wa Kiisiraeli na kuingia chumbani, walimolala, akawachoma wote wawili tumboni, yule mtu wa Kiisiraeli na huyo mwanamke; ndipo, pigo lilipokomeshwa kwao wana wa Isiraeli. Nao waliouawa na hilo pigo walikuwa watu 24000. Kisha Bwana akamwambia Mose kwamba: Pinehasi, mwana wa Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, ameyarudisha nyuma machafuko yangu makali, yawaondokee wana wa Isiraeli; kwani wivu, niliokuwa nao, uo huo ameuona naye katikati yao, kwa hiyo sikuwamaliza wana wa Isiraeli kwa wivu wangu. Kwa sababu hii umwambie: Vivi hivi ninamwekea agano la kumpatia utengemano. Yeye nao wa uzao wake watakaokuwako nyuma yake watakuwa wenye agano la utambikaji wa kale na kale, kwa kuwa aliona wivu kwa ajili ya Mungu wake, akawapatia wana wa Isiraeli upozi. Jina lake yule Mwisiraeli aliyekufa kwa kuuawa pamoja na yule mwanamke wa Kimidiani alikuwa Zimuri, mwana wa Salu, naye alikuwa mkuu wa mlango wa baba yake kwao Wasimeoni. Nalo jina lake yule mwanamke wa Kimidiani aliyeuawa alikuwa Kozibi, binti Suri aliyekuwa mkuu wa ukoo wa milango ya baba yake kwao Wamidiani. Kisha Bwana akamwambia Mose kwamba: Wainukieni Wamidiani, mwapige! Kwani ndio wanaowachukia ninyi kwa madanganyo yao walipowadanganya na matambiko ya Baali-Peori, tena wamewadanganya na kuwapa ndugu yao mke, yule Kozibi, binti mkuu wa Wamidiani, ni yule aliyeuawa siku hiyo, pigo lilipowapata kwa ajili ya Peori. Lile pigo lilipokwisha kukoma, Bwana akamwambia Mose na Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, kwamba: Toeni jumla yao wote walio mkutano wa wana wa Isiraeli kuanzia kwao walio wenye miaka ishirini na zaidi wa milango ya baba zao mkiwakagua wote wanaoweza kwenda vitani kwao Waisiraeli. Kwa hiyo Mose na mtambikaji Elazari wakasema nao kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili, kwamba: Wahesabuni wao walio wenye miaka ishirini na zaidi, kama Bwana alivyomwagiza Mose pamoja nao wana wa Isiraeli waliotoka katika nchi ya Misri. Rubeni, mwana wa kwanza wa Isiraeli, wanawe Rubeni walikuwa: Henoki, baba ya ndugu zao Wahenoki, Palu, baba ya ndugu zao Wapalu; Hesironi, baba ya ndugu zao Wahesironi, Karmi, baba ya ndugu zao Wakarmi. Hizi ndizo ndugu zao Warubeni, nao wa kwao waliokaguliwa walikuwa watu 43730. Wana wa Palu walikuwa wa Eliabu; nao hao wana wa Eliabu walikuwa Nemueli na Datani na Abiramu; nao Datani na Abiramu walikuwa wale wateule wa mkutano walioshindana na Mose na Haroni katika mkutano wao wa Kora, wao waliposhindana na Bwana. Ilikuwa hapo, nchi ilipoasama na kuwameza pamoja na Kora; wao wa mkutano wao walipokufa, moto ulikula watu 250, wakawa kielekezo cha kutisha. Lakini wana wa Kora hawakufa hapo. Wana wa Simeoni kwa ndugu zao walikuwa: Nemueli, baba ya ndugu zao Wanemueli, Yamini, baba ya ndugu zao Wayamini, Yakini, baba ya ndugu zao Wayakini, Zera, baba ya ndugu zao Wazera, Sauli baba ya ndugu zao Wasauli. Hizi ndizo ndugu zao Wasimeoni, watu 22200. Wana wa Gadi kwa ndugu zao walikuwa: Sefoni, baba ya ndugu zao Wasefoni, Hagi, baba ya ndugu zao Wahagi, Suni, baba ya ndugu zao Wasuni; Ozini, baba ya ndugu zao Waozini, Eri, baba ya ndugu zao Waeri; Arodi, baba ya ndugu zao Waarodi, Areli, baba ya ndugu zao Waareli. Hizi ndizo ndugu zao Wagadi; nao wa kwao waliokaguliwa walikuwa watu 40500. Wana wa Yuda walikuwa: Eri na Onani, nao Eri na Onani walikuwa wamekufa katika nchi ya Kanaani. Wana wa Yuda kwa ndugu zao walikuwa: Sela, baba ya ndugu zao Wasela, Peresi, baba ya ndugu zao Waperesi, Zera, baba ya ndugu zao Wazera. Nao wana wa Peresi walikuwa: Hesironi, baba ya ndugu zao Wahesironi, Hamuli, baba ya ndugu zao Wahamuli. Hizi ndizo ndugu zao Wayuda, nao wa kwao waliokaguliwa walikuwa watu 76500. Wana wa Isakari kwa ndugu zao walikuwa: Tola, baba ya ndugu zao Watola, Puwa, baba ya ndugu zao Wapuwa; Yasubu, baba ya ndugu zao Wayasubu, Simuroni, baba ya ndugu zao Wasimuroni. Hizi ndizo ndugu zao Waisakari, nao wa kwao waliokaguliwa walikuwa watu 64300. Wana wa Zebuluni kwa ndugu zao walikuwa: Seredi, baba ya ndugu zao Waseredi, Eloni, baba ya ndugu zao Waeloni, Yaleli, baba ya ndugu zao Wayaleli. Hizi ndizo ndugu zao Wazebuluni, nao wa kwao waliokaguliwa walikuwa watu 60500. Wana wa Yosefu kwa ndugu zao walikuwa: Manase na Efuraimu. Wana wa Manase walikuwa: Makiri, baba ya ndugu zao Wamakiri, naye Makiri akamzaa Gileadi, naye Gileadi alikuwa baba ya ndugu zao Wagileadi. Nao wana wa Gileadi walikuwa: Iezeri, baba ya ndugu zao Waiezeri, Heleki, baba ya ndugu zao Waheleki, na Asirieli, baba ya ndugu zao Waasirieli, na Sekemu, baba ya ndugu zao Wasekemu, na Semida, baba ya ndugu zao Wasemida, na Heferi, baba ya ndugu zao Waheferi. Lakini Selofuhadi, mwana wa Heferi, hakuwa na mwana wa kiume, walikuwa wa kike tu, nayo majina yao hao wana wa kike wa Selofuhadi yalikuwa Mala na Noa, Hogla, Milka na Tirsa. Hizi ndizo ndugu zao Wamanase, nao wa kwao waliokaguliwa walikuwa watu 52700. Wana wa Efuraimu kwa ndugu zao walikuwa: Sutela, baba ya ndugu zao Wasutela, Bekeri, baba ya ndugu zao Wabekeri, Tahani, baba ya ndugu zao Watahani. Nao hawa walikuwa wana wa Sutela: Erani, baba ya ndugu zao Waerani. Hizi ndizo ndugu zao wana wa Efuraimu, nao wa kwao waliokaguliwa walikuwa watu 32500. Hawa walikuwa wana wa Yosefu kwa ndugu zao. Wana wa Benyamini kwa ndugu zao walikuwa: Bela, baba ya ndugu zao Wabela, Asibeli, baba ya ndugu zao Waasibeli, Ahiramu, baba ya ndugu zao Waahiramu, Sufamu, baba ya ndugu zao Wasufamu, Hufamu, baba ya ndugu zao Wahufamu. Nao wana wa Bela walikuwa Ardi na Namani, baba ya ndugu zao Waardi na baba ya ndugu zao Wanamani. Hawa walikuwa wana wa Benyamini kwa ndugu zao, nao wa kwao waliokaguliwa walikuwa watu 45600. Hawa walikuwa wana wa Dani kwa ndugu zao: Suhamu, baba ya ndugu zao Wasuhamu; hizi ndizo ndugu zao Wadani kwa ndugu zao. Nao wa kwao ndugu zao Wasuhamu waliokaguliwa walikuwa watu 64400. Wana wa Aseri kwa ndugu zao walikuwa: Imuna, baba ya ndugu zao Waimuna, Iswi, baba ya ndugu zao Waiswi, Beria, baba ya ndugu zao Waberia. Wana wa Beria walikuwa: Heberi, baba ya ndugu zao Waheberi, Malkieli, baba ya ndugu zao Wamalkieli. Nalo jina la mwanawe wa kike wa Aseri alikuwa Sara. Hizi ndizo ndugu zao wana wa Aseri, nao wa kwao waliokaguliwa walikuwa watu 53400. Wana wa Nafutali kwa ndugu zao walikuwa: Yaseli, baba ya ndugu zao Wayaseli, Guni, baba ya ndugu zao Waguni, Yeseri, baba ya ndugu zao Wayeseri, Silemu, baba ya ndugu zao Wasilemu. Hizi ndizo ndugu zao Wanafutali kwa ndugu zao; nao wa kwao waliokaguliwa walikuwa watu 45400. Hii ilikuwa jumla ya wana wa Isiraeli waliokaguliwa watu 601730. Kisha Bwana akamwambia Mose kwamba: Hawa ndio watakaogawiwa nchi hiyo kwa hesabu ya majina. Walio wengi uwagawie fungu kubwa zaidi kuwa lao, nao walio wachache uwagawie fungu lililo dogo kidogo kuwa lao; kila shina sharti lipate fungu lake kwa hesabu yao waliokaguliwa kwake. Lakini nchi sharti igawanywe kwa kupiga kura, wapate mafungu yao kwa majina ya baba za mashina. Wao walio wengi nao walio wachache sharti mafungu yao ya kuwa yao wenyewe wagawiwe kwa kupigiwa kura. Nayo hii ndiyo jumla ya Walawi kwa ndugu zao: Gersoni, baba ya ndugu zao Wagersoni, Kehati, baba ya ndugu zao Wakehati, Merari baba ya ndugu zao Wamerari. Hizi ndizo ndugu zao Walawi: Ndugu zao Walibuni, ndugu zao Waheburoni, ndugu zao Wamahali, ndugu zao Wamusi, ndugu zao Wakora. Naye Kehati alimzaa Amuramu. Nalo jina lake mkewe Amuramu alikuwa Yokebedi, binti Lawi, huyu Lawi aliyezaliwa huko Misri, naye akamzalia Amuramu Haroni na Mose na umbu lao Miriamu. Naye Haroni aliwazaa: Nadabu na Abihu na Elazari na Itamari. Lakini Nadabu na Abihu walikufa walipomtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa isiyopasa. Jumla yao ilikuwa watu 23000, ndio wa kiume wote waliokuwa wenye mwezi mmoja na zaidi; kwani hawakukaguliwa katikati ya wana wa Isiraeli, kwa kuwa hawakupewa fungu lao wenyewe katikati ya wana wa Isiraeli. Hii ndiyo jumla yao, Mose na mtambikaji Elazari waliowakagua, walipowakagua wana wa Isiraeli kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili. Miongoni mwao hakuwamo mtu hata mmoja wao, Mose na mtambikaji Haroni waliowakagua walipowakagua wana wa Isiraeli nyikani kwa Sinai. Kwani Bwana aliwaambia: Hamna budi kufa nyikani; kwa hiyo hakusalia mtu hata mmoja kwao, ni Kalebu tu, mwana wa Yefune, na Yosua, mwana wa Nuni. Wakaja wana wa kike wa Selofuhadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, waliokuwa wa ndugu za Manase, mwana wa Yosefu, majina yao hawa wanawe wa kike ndiyo haya: Mala na Noa na Hogla na Milka na Tirsa. Hao wakamtokea Mose na mtambikaji Elazari na wakuu wa mkutano wote hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, wakasema: Baba yetu alikufa nyikani, naye hakuwa katika mkutano wao waliofanya shauri la kumpingia Bwana katika mkutano wao Wakora, ila alikufa kwa ukosaji wake yeye, lakini hakuwa na wana wa kiume. Mbona jina la baba yetu litoweke katika ndugu zake, kwa kuwa hakuwa na mwana wa kiume? Tupe sisi fungu katikati ya ndugu za baba yetu, tulichukue! Mose akalitokeza hilo shauri lao mbele ya Bwana. Naye Bwana akamwambia Mose kwamba: Haya, wana wa kike wa Selofuhadi waliyoyasema, ndiyo ya kweli. Uwape katikati ya ndugu za baba yao fungu, walichukue, liwe lao, ukiagiza, fungu la baba yao walipate wao. Nao wana wa Isiraeli waambie kwamba: Mtu akifa pasipo kuwa na mwana wa kiume, fungu lake huyu sharti mmwachie mwanawe wa kike. Kama hata mwana wa kike hakuwa naye, mtawapa ndugu zake fungu lake. Kama hata ndugu hakuwa nao, mtawapa ndugu za baba yake fungu lake. Kama baba yake hakuwa na ndugu, basi, hilo fungu lake mtampa ye yote aliye ndugu yake wa kuzaliwa naye wa mlango wake, alichukue. Haya na yawe kwao wana wa Isiraeli maongozi yenye haki, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Bwana akamwambia Mose: Panda huku juu mlimani kwa Abarimu, uitazame hiyo nchi, nitakayowapa wana wa Isiraeli. Ukiisha kuiona utachukuliwa nawe kwenda kwao walio ukoo wako, kama kaka yako Haroni alivyochukuliwa naye kwenda huko. Ni kwa kuwa nyikani kwa Sini hamkukitii vema kinywa changu cha kwamba: Mnitakase kwa kutoa maji machoni pao, mkutano huu uliponigombeza; hayo yalikuwa penye Maji ya Magomvi kule Kadesi nyikani kwa Sini. Naye Mose akamwambia Bwana kwamba: Bwana wangu aliye mwenye roho zao wote walio wenye miili na aweke mtu kuwa mkuu wa mkutano huu, atakayewatangulia kwa kutoka na kuingia kwake, atakayewaongoza wao, wapate kutoka na kuingia tena, watu wa mkutano huu wa Bwana wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo, Bwana alipomwambia Mose: Mchukue Yosua, mwana wa Nuni, aliye mtu mwenye Roho yangu moyoni mwake, umbandikie mkono kichwani pake! Kisha msimamishe mbele ya mtambikaji Elazari machoni pao walio wa mkutano huu, umwagizie mambo yako machoni pao na kumgawia utukufu wako, umkalie naye, watu wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli wamsikie. Itakapotukia, na amtokee mtambikaji Elazari, ampigie bao na kuutumia Urimu mbele ya Bwana, kama desturi; utakaposema, watoke, sharti watoke, tena utakaposema, waingie, sharti waingie, yeye na wana wote wa Isiraeli pamoja naye, huo mkutano wote pia. Mose akafanya, kama Bwana alivyomwagiza: akamchukua Yosua, akamsimamisha mbele ya mtambikaji Elazari na mbele ya mkutano wote. Kisha akambandikia mikono yake kichwani pake, akamwagizia mambo yake, kama Bwana alivyosema kinywani mwa Mose. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waagize wana wa Isiraeli, uwaambie: Jiangalieni, mnitolee wakati huo uliowekwa matoleo yanayonipasa, ndio chakula changu cha ng'ombe za tambiko zinazoteketezwa kuwa mnuko wa kunipendeza. Uwaambie: Nazo hizi ndizo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa, mtakazomtolea Bwana: Wana kondoo wa mwaka mmoja wasio na kilema, pasipo kukoma kila siku wawili kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima. Mwana kondoo mmoja utamtoa asubuhi, naye mwana kondoo wa pili utamtoa saa za jioni. Pamoja naye utoe vibaba vitatu vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na kibaba kimoja cha mafuta yaliyotwangwa vema kuwa kilaji cha tambiko. Hii ndio ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima iliyotolewa kila siku mlimani kwa Sinai kuwa moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Tena utoe kinywaji chake cha tambiko, kibaba kimoja cha mvinyo kwa kila mwana kondoo, nacho hicho kinywaji cha tambiko cha mvinyo yenye nguvu ummiminie Bwana hapo Patakatifu. Naye mwana kondoo wa pili na umtoe saa za jioni pamoja na kilaji cha tambiko na kinywaji chake cha tambiko kama asubuhi; ukifanya hivyo, vitakuwa moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Tena siku ya mapumziko mtoe wana kondoo wawili wa mwaka mmoja wasio na kilema na vibaba sita vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko, tena kinywaji chake cha tambiko. Hizi ndizo ng'ombe za tambiko za kila siku ya mapumziko, mtakazozitoa pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kila siku na kinywaji chake cha tambiko. Tena siku za kwanza za miezi yenu na mmtolee Bwana kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima: madume mawili ya ng'ombe walio vijana bado na dume moja la kondoo na wana kondoo saba wa mwaka mmoja wasio na kilema. Tena mtoe vibaba tisa vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko cha dume moja la ng'ombe na vibaba sita vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko cha dume moja la kondoo. Tena vibaba vitatutatu vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko cha kila mwana kondoo mmoja. Ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima itakayotolewa hivyo itakuwa moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Navyo vinywaji vyao vya tambiko na viwe vibaba viwili vya mvinyo vya dume moja la ng'ombe na kibaba kimoja na nusu cha mvinyo cha dume la kondoo na kibaba kimoja cha mvinyo cha mwana kondoo mmoja. Hizi ndizo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima za mwandamo wa mwezi, mtakazozitoa mwezi kwa mwezi mwaka mzima. Tena pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku Bwana na atolewe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na kinywaji chake cha tambiko. Siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza ni Pasaka ya Bwana. Siku ya kumi na tano ya mwezi huo na mle sikukuu; ndipo iliwe mikate isiyochachwa siku saba. Siku ya kwanza na mkutanie Patakatifu, msifanye kazi yo yote ya utumishi, ila mmtolee Bwana kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima motoni: madume mawili ya ng'ombe walio vijana bado na dume moja la kondoo na wana kondoo saba wa mwaka mmoja wasio na kilema; hawa ndio, mtakaowatoa. Navyo vilaji vyao vya tambiko na mtoe vibaba tisa vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta vya dume moja la ng'ombe na vibaba sita vya dume la kondoo. Tena na mtoe vibaba vitatutatu vya kila mwana kondoo mmoja wa wale wana kondoo saba. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo kuwapatia ninyi upozi. Hao sharti mwatoe pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya asubuhi inayotolewa kila siku. Hao na mwatoe kila siku siku hizo saba kuwa chakula cha moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana; nao na watolewe pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku pamoja na kinywaji chake cha tambiko. Siku ya saba na mkutanie Patakatifu, msifanye kazi yo yote ya utumishi. Siku ya malimbuko, mtakapomtolea Bwana vilaji vipya vya tambiko, ndio sikukuu yenu ya majuma saba; hapo na mkutanie Patakatifu, msifanye kazi yo yote ya utumishi. Tena na mtoe kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, ziwe mnuko wa kumpendeza Bwana: madume mawili ya ng'ombe walio vijana bado na dume moja la kondoo na wana kondoo saba wa mwaka mmoja. Navyo vilaji vyao vya tambiko na viwe vibaba tisa vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta vya dume moja la ng'ombe na vibaba sita vya dume moja la kondoo, tena vibaba vitatutatu vya kila mwana kondoo mmoja wa wale wana kondoo saba. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwapatia ninyi upozi. Hao na mwatoe pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku pamoja na kilaji chake cha tambiko; nao sharti wawe pasipo kilema, tena mtoe navyo vinywaji vyao vya tambiko. Siku ya kwanza ya mwezi wa saba na mkutanie Patakatifu, msifanye kazi yo yote ya utumishi, iwe sikukuu yenu ya Shangwe. Hapo na mtoe kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, ziwe mnuko wa kumpendeza Bwana: dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na wana kondoo saba wa mwaka mmoja wasio na kilema. Navyo vilaji vyao vya tambiko na viwe vibaba tisa vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta vya dume la ng'ombe na vibaba sita vya dume la kondoo, na vibaba vitatu vya kila mwana kondoo mmoja wa wale wana kondoo saba. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo kuwapatia ninyi upozi. Hao na mtoe pamoja na ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima za mwandamo wa mwezi pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku pamoja na vilaji vyake vya tambiko, tena na mvitoe navyo vinywaji vyao vya tambiko, kama ilivyo desturi yao kuwa moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana. Siku ya kumi ya mwezi huo wa saba na mkutanie Patakatifu na kujitesa kwa kufunga, msifanye kazi yo yote, ila mtolee Bwana kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, ziwe mnuko wa kumpendeza: dume moja la ng'ombe aliye kijana bado na dume moja la kondoo na wana kondoo saba wa mwaka mmoja wasio na kilema; hawa ndio, mtakaowatoa. Navyo vilaji vyao vya tambiko na viwe vibaba tisa vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta vya dume la ng'ombe na vibaba sita vya dume moja la kondoo, na vibaba vitatutatu vya kila mwana kondoo mmoja wa wale wana kondoo saba. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ng'ombe ya tambiko ya weuo ya sikukuu ya Mapoza na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku pamoja na vilaji vyake vya tambiko, tena na mvitoe navyo vinywaji vyao ya tambiko. Siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba na mkutanie Patakatifu, msifanye kazi yo yote ya utumishi, ila mzile hizo sikukuu za Bwana siku saba. Hapo na mtoe ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, ziwe moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana: madume kumi na matatu ya ng'ombe walio vijana bado na madume mawili ya kondoo na wana kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja wasio na kilema. Navyo vilaji vyao vya tambiko na viwe vibaba tisa vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na mafuta vya dume moja la ng'ombe wa wale madume ya ng'ombe kumi na matatu na vibaba sita vya dume moja la kondoo wa wale madume mawili ya kondoo, na vibaba vitatutatu vya kila mwana kondoo mmoja wa wale wana kondoo kumi na wanne. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku, tena na mvitoe navyo vilaji na vinywaji vyake vya tambiko. Siku ya pili na mtoe madume kumi na mawili ya ng'ombe walio vijana bado na madume mawili ya kondoo na wana kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja wasio na kilema. Navyo vilaji na vinywaji vyao vya tambiko vya madume ya ng'ombe navyo vya madume ya kondoo navyo vya wana kondoo na mvitoe kwa hesabu yao kama desturi. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku pamoja na vilaji vyake vya tambiko, tena na mvitoe navyo vinywaji vyao vya tambiko. Siku ya tatu na mtoe madume kumi na moja ya ng'ombe na madume mawili ya kondoo na wana kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja wasio na kilema. Navyo vilaji na vinywaji vya tambiko vya madume ya ng'ombe, navyo vya madume ya kondoo, navyo vya wana kondoo na mvitoe kwa hesabu yao kama desturi. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ng'ombe ya tambik ya kuteketezwa nzima ya kila siku, tena na mvitoe navyo vilaji na vinywaji vyake vya tambiko. Siku ya nne na mtoe madume kumi ya ng'ombe na madume mawili ya kondoo na wana kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja wasio na kilema. Navyo vilaji na vinywaji vyao vya tambiko vya madume ya ng'ombe, navyo vya madume ya kondoo, navyo vya wana kondoo na mvitoe kwa hesabu yao kama desturi. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku, tena na mvitoe navyo vilaji na vinywaji vyake vya tambiko. Siku ya tano na mtoe madume tisa ya ng'ombe na madume mawili ya kondoo na wana kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja wasio na kilema. Navyo vilaji na vinywaji vyao vya tambiko vya madume ya ng'ombe, navyo vya madume ya kondoo, navyo vya wana kondoo na mvitoe kwa hesabu yao kama desturi. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku, tena na mvitoe navyo vilaji na vinywaji vyake vya tambiko. Siku ya sita na mtoe madume manane ya ng'ombe na madume mawili ya kondoo na wana mbuzi kumi na wanne wa mwaka mmoja wasio na kilema. Navyo vilaji na vinywaji vyao vya tambiko vya madume ya ng'ombe, navyo vya madume ya kondoo, navyo vya wana kondoo na mvitoe kwa hesabu yao kama desturi. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku, tena na mvitoe navyo vilaji na vinywaji vyake vya tambiko. Siku ya saba na mtoe madume saba ya ng'ombe na madume mawili ya kondoo na wana kondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja wasio na kilema. Navyo vilaji na vinywaji vyao vya tambiko vya madume ya ng'ombe, navyo vya madume ya kondoo, navyo vya wana kondoo na mvitoe kwa hesabu yao kama desturi. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku, tena na mvitoe navyo vilaji na vinywaji vyake vya tambiko. Siku ya nane na iwe ya mkutano mkuu kwenu, msifanye kazi yo yote ya utumishi, ila mtoe ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, ziwe moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana: dume moja la ng'ombe na dume moja la kondoo na wana kondoo saba wa mwaka mmoja wasio na kilema. Navyo vilaji na vinywaji vyote vya tambiko vya yule dume la ng'ombe, navyo vya yule dume la kondoo, navyo vya wale wana kondoo na mvitoe kwa hesabu yao kama desturi. Tena na mtoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ya kila siku, tena na mvitoe navyo vilaji na vinywaji vyake vya tambiko. Hizo ndizo ng'ombe za tambiko, mtakazomtolea Bwana, sikukuu zenu zitakapotimia; tena ziko zile, mtakazozitoa kwa kuapa au kwa kupenda wenyewe kuwa ng'ombe zenu za tambiko za kuteketezwa nzima au vilaji au vinywaji vyenu vya tambiko au ng'ombe zenu za tambiko za shukrani. Mose akawaambia wana wa Isiraeli haya yote, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Mose akawaambia wakuu wa mashia ya wana wa Isiraeli kwamba: Hili ndilo neno, Bwana aliloliagiza: Mtu akimwapia Bwana kumtolea cho chote au kiapo cha kujifungia kifungo cho chote, asilitangue neno lake, ila sharti ayafanye yote, kama kinywa chake kilivyoyasema. Mwanamke akimwapia Bwana kumtolea cho chote, au akijifungia kiungo, akingali nyumbani mwa baba yake, au akingali kijana bado, naye baba yake akipata habari ya kule kuapa kwake au ya kujifungia kifungo cho chote, basi, baba yake akimnyamazia kimya, yote aliyoyaapa yatakuwapo, navyo vifungo vyote, alivyojifungia, vitakuwa vimemfunga. Lakini baba yake akimkataza siku hiyo, anapopata habari, basi, yote aliyoyaapa navyo vifungo vyote, alivyojifungia, havitakuwapo, naye Bwana atamwondolea jambo hilo, kwa kuwa baba yake amemkataza. Lakini atakapoolewa akiwa mwenye mambo, aliyoyaapa, au midomo yake iliyojisemea tu ya kjifungia kifungo, basi, mumewe akipata habari na kumnyamazia kimya siku hiyo, anapopata habari, yatakuwapo aliyoyaapa, navyo vifungo, alivyojifungia, vitakuwapo. Lakini mumewe akimkataza siku hiyo, anapopata habari, basi, yeye atakuwa ameyatangua hayo mambo, aliyokuwa nayo kwa kuapa, nayo yale, midomo yake iliyojisemea tu ya kujifungia kifungo, naye Bwana atamwondolea jambo hilo. Lakini mjane au mwanamke aliyeachana na mumewe atakayoyaapa navyo vifungo vyote, atakavyojifungia, vitakuwapo, vimfunge. Mwanamke akijiapia mambo yo yote nyumbani mwa mumewe au akijifungia kifungo cho chote kwa kiapo, basi, mumewe akipata habari yake na kumnyamazia kimya, asimkataze, yote aliyoyaapa yatakuwapo, navyo vifungo vyote, alivyojifungia, vitakuwapo. Lakini mumewe akivitangua kabisa siku hiyo, anapopata habari, basi, yote yaliyotoka midomoni mwa mkewe ya kiapo nayo ya kujifungia kifungo hayatakuwapo, kwa kuwa mumewe ameyatangua, naye Bwana atamwondolea jambo hilo. Yote, mwanamke aliyoyaapa, navyo vifungo vyote, alivyojifungia kwa kiapo vya kujiumiza mwenyewe, mumewe anaweza kuyatia nguvu, yawepo, tena mumewe anaweza kuyatangua. Mumewe akimnyamazia kimya tangu leo hata kesho, basi, amekwisha kuyatia nguvu, yawepo yote, aliyoyaapa, navyo vifungo vyote, alivyojifungia, amekwisha kuvitia nguvu navyo, viwepo, kwani amemnyamazia kimya siku hiyo, alipopata habari. Naye akiisha kupata habari, tena akivitangua siku za nyuma hana budi kujitwika manza za mkewe. Haya ndiyo maongozi, Bwana aliyomwagiza Mose ya kuwaongoza mtu na mkewe, hata baba na mwanawe wa kike, akiwa angaliko kijana na kukaa nyumbani mwa baba yake. Bwana akamwambia Mose kwamba: Walipizie wana wa Isiraeli kwa Wamidiani! Kisha utachukuliwa kwenda kwao walio ukoo wako. Ndipo, Mose alipowaambia watu kwamba: Tengenezeni watu wa kwenu kwenda vitani, wawaendee Wamidiani kumpatia Bwana lipizo kwao Wamidiani! Kwao mashina ya Waisiraeli kila shina moja litoe watu elfu moja na kuwatuama kwenda vitani. Kwa hiyo wakatolewa katika maelfu ya Waisiraeli elfu moja katika kila shina, wakawa watu maelfu kumi na mawili waliotengenezwa kwenda vitani. Hayo maelfu, elfu moja la kila shina, Mose akawatuma kwenda vitani pamoja na Pinehasi, mwana wa mtambikaji Elazari; huyu alishika mkononi mwake vyombo vya Patakatifu nayo yale matarumbeta ya shangwe. Wakaenda vitani kupigana na adui, kama Bwana alivyomwagiza Mose, wakawaua wa kiume wote. Nao wafalme wa Wamidiani wakawaua pamoja na watu wao waliouawa: Ewi na Rekemu na Suri na Huri na Reba; hao watano ndio waliokuwa wafalme wao Wamidiani. Naye Bileamu, mwana wa Beori, wakamwua kwa upanga. Kisha wana wa Isiraeli wakawateka wanawake wa Midiani na watoto wao, nao ng'ombe wao wote na mbuzi na kondoo wao wote na mali zao zote pia wakazichukua kuwa nyara zao. Lakini miji yao yote, walimokaa, na makambi yenye mahema yao wakayateketeza kwa moto. Kisha wakawachukua nyama wote na mateka yote, watu pamoja na nyama, wote pia wakawapeleka kwa Mose na kwa mtambikaji Elazari na kwao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli; mateka na mapato ndiyo, waliyoyapeleka pamoja na nyara makambini kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani; ndipo hapo, Yeriko ulipokuwa ng'ambo ya pili. Ndipo, Mose na mtambikaji Elazari na wakuu wote wa mkutano walipotoka kwenda kukutana nao huko nje ya makambi. Lakini Mose akawakasirikia waliowekwa kuvisimamia vikosi, wale wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia waliotoka kwa kupiga vita; kwa hiyo Mose akawaambia: Kumbe mmewaponya wanawake wote! Nao ndio walioongozwa na Bileamu, wakawakosesha wana wa Isiraeli, wamvunjie Bwana maagano kwa ajili ya Peori, nao wa mkutano wa Bwana wakapatwa na pigo kwa sababu hiyo. Sasa waueni watoto wa kiume wote! Nao wanawake wote wanaojua waume kwa kulala nao wa kiume waueni nao! Lakini watoto wa kike wote wasiojua bado kulala nao wa kiume waponyeni, wakae kwenu! Kisha ninyi laleni nje ya makambi siku saba, ninyi nyote mlioua mtu nanyi mliogusa tu mtu aliyeuawa, mjieue siku ya tatu na siku ya saba, ninyi wenyewe pamoja na mateka yenu. Nazo nguo zote navyo vyombo vyote vya ngozi navyo vyote vilivyotengenezwa kwa manyoya ya singa za mbuzi navyo vyombo vyote vya mti sharti mvieue. Naye mtambikaji Elazari akawaambia askari waliotoka kwa kupiga vita: Haya ndiyo maongozi ya maonyo, Bwana aliyomwagiza Mose: vilivyo dhahabu na fedha na shaba na vyuma na mabati na risasi, navyo vyote vinavyoweza kuingia motoni sharti mvipitishe motoni, vipate kutakata, kisha mvieue kwa yale maji ya kunyunyiza; lakini vyote visivyopatana na moto na mvipitishe majini. Kisha sharti mzifue nguo zenu siku ya saba; ndipo, mtakapokuwa wenye kutakata, baadaye mtaingia makambini. Bwana akamwambia Mose kwamba: Toa jumla yao mateka, waliyoyapata ya watu na ya nyama, wewe pamoja na mtambikaji Elazari nao wakuu wa milango ya mkutano! Kisha hayo mapato uyatoe mafungu mawili, moja liwe lao walioshika kazi ya mapigano na kwenda vitani, la pili liwe lao wengine wote wa mkutano. Kisha wao waliokwenda kupiga vita uwatoze toleo limpasalo Bwana: kwa kila mia tano mmoja, kama ni watu au ng'ombe au punda au mbuzi au kondoo. Hivyo ndivyo, utakavyowatoza katika nusu yao, umpe mtambikaji Elazari kuwa vipaji vya tambiko vya kumnyanyulia Bwana. Lakini katika nusu yao wana wa Isiraeli uchukue mmoja na kumtoa katika kila hamsini, kama ni watu au ng'ombe au punda au mbuzi au kondoo; katika nyama wote utoe hivyo, uwape Walawi wanaongoja zamu ya kuliangalia Kao la Bwana. Ndipo, Mose na mtambikaji Elazari walipofanya, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Masao ya nyara, watu wa vita walizozichukua, mapato hayo yalikuwa mbuzi na kondoo pamoja 675000, na ng'ombe 72000, na punda 61000. Nao wana wa kike wasiojua bado kulala na mtu wa kiume wote pamoja walikuwa 32000. kwa hiyo ile nusu iliyokuwa fungu lao waliokwenda vitani, hesabu ya mbuzi na kondoo ilikuwa 337500. Nalo toleo lililompasa Bwana la hao mbuzi na kondoo lilikuwa 675. Nao ng'ombe wao walkuwa 36000, nalo toleo lao lililompasa Bwana lilikuwa ng'ombe 72. Nao punda walikuwa 30500, nalo toleo lao lililompasa Bwana lilikuwa 61. Nao watu wao walikuwa 16000, nalo toleo lao lililompasa Bwana lilikuwa watu 32. Hayo matoleo Mose akampa mtambikaji Elazari kuwa vipaji vya tambiko vya kumnyanyulia Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Nayo nusu nyingine ya wana wa Isiraeli, Mose aliyoiondoa kwao waliokwenda kuvipiga hivyo vita, hiyo nusu iliyokuwa yao wa mkutano ilikuwa nayo mbuzi na kondoo 337500, nao ng'ombe walikuwa 36000, nao punda walikuwa 30500, nao watu walikuwa 16000. Katika nusu hii ya wana wa Isiraeli Mose akachukua mmoja aliyetolewa katika kila hamsini, kama ni watu au nyama, akawapa Walawi waliongoja zamu ya kuliangalia Kao la Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kisha waliowekwa kuyasimamia maelfu ya vikosi, wale wakuu wa maelfu na wa mamia wakamkaribia Mose, wakamwambia Mose: Sisi watumishi wako tumetoa jumla ya watu wa vita, tuliowashika mikononi mwetu, namo miongoni mwao hakukoseka hata mmoja. Kwa hiyo tunamtolea Bwana vyombo vya dhahabu, kila mtu alivyoviona kuwa matoleo: vikuku na vitimbi na pete za vidoleni na mapete ya masikioni na mapambo yo yote, tujipatie upozi mbele ya Bwana. Mose na mtambikaji Elazari wakachukua kwao hizo dhahabu zilizotengenezwa kuwa hivyo vyombo vyote. Nazo dhahabu zote, walizomtolea Bwana kuwa vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa zilikuwa frasila kumi na saba, ndizo zilizotoka kwa wakuu wa maelfu na kwa wakuu wa mamia. Nao waliokuwa askari tu walijichukulia kila mtu nyara zake. Mose na mtambikaji Elazari walipokwisha kuzichukua hizo dhahabu kwao wakuu wa maelfu na wa mamia wakazipeleka Hemani wa Mkutano, ziwe za kumkumbusha Bwana, asikoe kuwatazama wana wa Iiraeli. Wana wa Rubeni na wana wa Gadi walikuwa na nyama wa kufuga wengi sanasana; walipoitazama nchi ya Yazeri na nchi ya Gileadi wakaziona kuwa zenye mahali pengipengi panapofaa pa kufugia nyama. Kwa hiyo wana wa Gadi na wana wa Rubeni wakamjia Mose na mtambikaji Elazari na wakuu wa mkutano, wakawaambia: Ataroti na Diboni na Yazeri na Nimura na Hesiboni na Elale na Sibamu na Nebo na Beoni, hizi nchi, Bwana alizozipiga mbele ya mkutano wa Isiraeli, ni nchi zifaazo kwa kufuga nyama, nasi watumishi wako tunao nyama wa kufuga. Wakasema: Kama tumeona upendeleo machoni pako, sisi watumishi wako, na tupewe nchi hizi, tuzichukue, usituvukishe mto wa Yordani! Ndipo, Mose alipowaambia wana wa Gadi na wana wa Rubeni: Mbona mnataka, ndugu zenu waende vitani, ninyi mkikaa hapo? Mbona mnataka kuikataza mioyo ya wana wa Isiraeli, wasivuke na kuiingia nchi, Bwana aliyowaapia? Hivi ndivyo, baba zenu walivyofanya, nilipowatuma toka Kadesi-Barnea kwenda kuitazama nchi hii. Walipokwisha kupanda na kufika kwenye kijito cha Eskoli na kuiona nchi hii, wakaikataza mioyo yao wana wa Isiraeli, wasiingie katika nchi hiyo, Bwana aliyowapa. Siku hiyo makali ya Bwana yakawaka, akaapa kwamba: Watu hawa waliotoka Misri kufika huku walio wenye miaka ishirini na zaidi hawataiona kabisa nchi hiyo, niliyowaapia Aburahamu na Isaka na Yakobo, kwa kuwa hawakunifuata kwa mioyo yote. Ila Kalebu, mwana wa Mkenizi Yefune, na Yosua, mwana wa Nuni, hawa tu wataiingia, kwa kuwa wamemfuata Bwana kwa mioyo yote. Kwa kuwa makali ya Bwana yaliwawakia wana wa Isiraeli, akawatembeza nyikani miaka 40, mpaka kimalizike kile kizazi chao chote walioyafanya hayo yaliyokuwa mabaya machoni pake Bwana. Sasa ninawaona ninyi, ya kama mmeinuka mahali pa baba zenu na kujitokeza kuwa wana wao wale wakosaji, mwuongeze moto wa makali ya Bwana, uzidi kuwawakia wana wa Isiraeli. Mkirudi nyuma na kumwacha, naye atawaacha tena siku nyingi nyikani; ndivyo, mtakavyowaangamiza hawa watu wote pia. Ndipo, walipomkaribia, wakamwambia: Tunataka tu kujenga huku mazizi ya nyama wetu wa kufuga na miji ya watoto wetu. Kisha sisi wenyewe tutajitengeneza upesi kuwatangulia wana wa Isiraeli, mpaka tuwaingize mahali pao, watoto wetu wakikaa katika miji yenye maboma kwa ajili ya wenyeji wa nchi hii. Hatutarudi nyumbani kwetu, mpaka wana wa Isiraeli watakapokwisha kupata kila mtu fungu lake mwenyewe. Kwani sisi hatutapata mafungu pamoja nao ng'ambo ya huko ya Yordani pande hizo za huko, kwani mafungu yetu sisi yametuangukia ng'ambo ya huku ya Yordani upande wa maawioni kwa jua. Ndipo, Mose alipowaambia: Mkilifanya neno hili na kujitengeneza kwenda vitani mbele ya Bwana, nanyi nyote mkiuvuka Yordani mbele ya Bwana na kushika mata ya vita, mpaka awafukuze adui zake mbele yake, nayo nchi hiyo itiishwe mbele ya Bwana, basi, baadaye mtarudi mkiwa watu wasiomkosea Bwana, wasiowakosea nao Waisiraeli; ndipo, nchi hii itakapokuwa yenu, mwichukue mbele ya Bwana, iwe yenu kabisa. Lakini msipovifanya hivyo, mtajiona kuwa watu waliomkosea Bwana, tena mtajua, ya kuwa makosa yenu yatawapata! Basi, wajengeeni watoto wenu miji nayo makundi yenu mazizi, kisha yafanyeni mliyoyasema kwa vinywa vyenu! Ndipo, wana wa Gadi na wana wa Rubeni walipomwambia Mose kwamba: Watumishi wako watafanya, kama bwana wetu anavyoagiza. Watoto wetu na wake zetu na mbuzi na kondoo wetu na nyama wetu wengine wa kufuga watakaa huku katika miji ya Gileadi, lakini watumishi wako wote wanaoweza kushika mata na kwenda vitani watavuka machoni pa Bwana kwenda kupigana, kama bwana wetu alivyosema. Kisha Mose akamwagiza mtambikaji Elazari na Yosua, mwana wa Nuni, na wakuu wa milango ya mashina ya wana wa Isiraeli, yeye Mose akiwaambia: Wana wa Gadi na wana wa Rubeni, ni kwamba: wote wa kwao wanaoweza kushika mata ya vita wakiuvuka Yordani pamoja nanyi machoni pa Bwana, basi, nchi itakapokuwa imetiishwa mbele yenu, sharti mwape nchi hii ya Gileadi, waichukue, iwe yao. Lakini wa kwao wanaoweza kushika mata wasipovuka pamoja nanyi, basi, na wapate mafungu yao katikati yenu katika nchi ya Kanaani. Nao wana wa Gadi na wana wa Rubeni wakaitikia kwamba: Kama Bwana alivyowaambia watumishi wako, ndivyo, tutakavyofanya. Sisi tunaoweza kushika mata tutavuka machoni pa Bwana kuingia katika nchi ya Kanaani, lakini mafungu yetu sisi, tutakayoyachukua, yawe yetu wenyewe, yatakuwa ng'ambo ya huku ya Yordani. Ndipo, Mose alipowapa wana wa Gadi na wana wa Rubeni nao wa nusu ya shina la Manase, mwana wa Yosefu, ufalme wa Sihoni, mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogi, mfalme wa Basani; nchi hii yote pamoja na miji yake yote pia iliyokuwamo katika mipaka yake iliyoizunguka nchi hiyo. Ndipo, wana wa Gadi walipoijenga miji ya Diboni na Ataroti na Aroeri, na Ataroti-Sofani na Yazeri na Yogibeha na Beti-Nimura na Beti-Harani; nayo ilikuwa miji yenye maboma na mazizi ya makundi. Nao wana wa Rubeni wakaijenga miji ya Hesiboni na Elale na Kiriataimu na Nebo na Baali-Meoni, wakiligeuza jina lake, na Sibuma; ndiyo majina, waliyoiita hiyo miji, waliyoijenga. Nao wana wa Makiri, mwana wa Manase, wakaenda Gileadi, wakauteka wakiwafukuza Waamori waliokaa humo. Kisha Mose akampa Makiri, mwana wa Manase, mji wa Gileadi, akakaa humo. Naye Yairi, mwana wa Manase, akaenda, akaviteka vijiji vyao vya mahema, akaviita vijiji vya Mahema ya Yairi. Naye Noba akaenda, akauteka Kenati na mitaa yake, akauita kwa jina lake Noba. Hizi ndizo safari za wana wa Isiraeli, vikosi vyao vilipotoka katika nchi ya Misri, wakiongozwa na Mose na Haroni. Mose akaziandika hizo safari zao, kama walivyotoka na kuondoka kwa kuagizwa na Bwana, nayo haya ndiyo matuo yao, walipoondoka kwendelea katika safari zao: siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza, ndiyo siku ya pili ya Pasaka, ndipo, wana wa Isiraeli walipoondoka Ramusesi machoni pao Wamisri wote kwa nguvu za mkono uliotoka juu. Nao Wamisri walikuwa wakiwazika wana wao wote wa kwanza, Bwana aliowapiga kwao, kwani Bwana aliihukumu miungu yao. Wana wa Isiraeli walipoondoka Ramusesi wakapiga makambi Sukoti. Walipoondoka sukoti wakapiga makambi Etamu ulioko kwenye mapeo ya nyika. Walipoondoka Etamu wakarudi Pi-Hahiroti unaoelekea Baali-Sefoni, wakapiga makambi mbele ya Migidoli. Walipoondoka mbele yake Hahiroti wakapita katikati ya bahari, wakaingia nyikani; walipokwenda safari ya siku tatu katika nyika ya Etamu wakapiga makambi Mara. Walipoondoka Mara wakafika Elimu; nako huko Elimu kulikuwa na visima vya maji 12 na mitende 70; kwa hiyo walipiga makambi huko. Waalipondoka Elimu wakapiga makambi kwenye Bahari Nyekundu. Walipoondoka kwenye Bahari Nyekundu wakapiga makambi nyikani kwa Sini. Walipoondoka nyikani kwa Sini wakapiga makambi Dofuka. Walipoondoka Dofuka wakapiga makambi Alusi. Walipoondoka Alusi wakapiga makambi Refidimu; huko ndiko, watu walikokosa maji ya kunywa. Walipoondoka Refidumu wakapiga makambi nyikani kwa Sinai. Walipoondoka nyikani kwa Sinai wakapiga makambi kwenye Makaburi ya Uchu. Walipoondoka kwenye Makaburi ya Uchu, wakapiga makambi Haseroti. Walipoondoka Haseroti wakapiga makambi Ritima. Walipoondoka Ritima wakapiga makambi Rimoni-Peresi. Walipoondoka Rimoni-Peresi wakapiga makambi Libuna. Walipoondoka Libuna wakapiga makambi Risa. Walipoondoka Risa wakapiga makambi Kehelata. Walipoondoka Kehelata wakapiga makambi mlimani kwa Seferi. Walipoondoka mlimani kwa Seferi wakapiga makambi Harada. Walipoondoka harada wakapiga makambi Makeloti. Walipoondoka Makeloti wakapiga makambi Tahati. Walipoondoka Tahati wakapiga makambi Tara. Walipoondoka Tara wakapiga makambi Mitika. Walipoondoka Mitika wakapiga makambi Hasimona. Walipoondoka Hasimona wakapiga makambi Moseroti. Walipoondoka Moseroti wakapiga makambi kwa wana wa Yakani. Walipoondoka kwa wana wa Yakani wakapiga makambi Hori-Hagidigadi. Walipoondoka Hori-Hagidigadi wakapiga makambi Yotibata. Walipoondoka Yotibata wakapiga makambi Aburona. Walipoondoka Aburona wakapiga makambi Esioni-Geberi. Walipoondoka Esioni-Geberi wakapiga makambi nyikani kwa Sini, ndio Kadesi. Walipoondoka Kadesi wakapiga makambi mlimani kwa Hori kwenye mwisho wa nchi ya Edomu. Ndipo, mtambikaji Haroni alipopanda mlimani kwa Hori kwa kuagizwa na Bwana, akafa huko siku ya kwanza ya mwezi wa tano katika mwaka wa arobaini tangu hapo, wana wa Isiraeli walipotoka katika nchi ya Misri; naye alikuwa mwenye miaka 123, alipokufa mlimani kwa Hori. Ndipo, Aradi, mfalme wa Kanaani, aliposikia, ya kuwa wana wa Isiraeli wanakuja; maana alikaa upande wa kusini wa nchi ya Kanaani. Walipoondoka mlimani kwa Hori wakapiga makambi Salmona. Walipoondoka Salmona wakapiga makambi Punoni. Walipoondoka Punoni wakapiga makambi Oboti. Walipoondoka Oboti wakapiga makambi Iye-Abarimu mpakani kwa Moabu. Walipoondoka huko Iyimu wakapiga makambi Diboni wa Gadi. Walipoondoka Diboni wa Gadi wakapiga makambi Almoni-Dibulataimu. Walipoondoka Almoni-Dibulataimu wakapiga makambi milimani kwa Abarimu kunakoelekea Nebo. Walipoondoka milimani kwa Abarimu wakapiga makambi kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili. Huko Yordani ndiko, walikopiga makambi kutoka Beti-Yesimoti mpaka Abeli-Sitimu kwenye mbuga za Moabu. Bwana akamwambia Mose huko kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili, kwamba: Sema na wana wa Isiraeli, uwaambie: Mtakapouvuka Yordani kuingia katika nchi ya Kanaani. sharti mwafukuze mbele yenu wenyeji wote wa nchi hiyo, kisha myaharibu mawe yao yote yenye machorochoro ya kuyaangukia, navyo vinyago vyao vyote vilivyoyeyushwa sharti mviharibu, napo pao pote pa kutambikia vilimani sharti mpabomoe. Kisha mtaichukua hiyo nchi, mkae huko, kwani nimewapa ninyi nchi hiyo, mwichukue, iwe yenu. Nayo nchi mtaigawanyia ndugu zenu kwa kupiga kura; ndugu walio wengi mwagawie fungu kubwa zaidi kuwa lao, nao walio wachache mwagawie fungu lililo dogo kidogo kuwa lao. Huko, kura itakakomwangukia kila mtu, kutakuwa kwake; sharti mgawiane mafungu yenu kwa mashina ya baba zao. Lakini msipowafukuza mbele yenu wenyeji wa nchi hiyo, basi, hao mtakaowasaza watakuwa miiba machoni penu na machomo mbavuni penu, wawasonge ninyi katika nchi, mtakayoikaa ninyi. Mwisho utakuwa, niwafanyizie ninyi yaleyale, niliyoyawaza kuwafanyizia wao. Bwana akamwambia Mose kwamba: Waagize wana wa Isiraeli, uwaambie: Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani, basi, nchi itakayowaangukia kuwa fungu lenu itakuwa nchi ya Kanaani hivyo, ilivyo na mipaka yake. Mpaka wenu wa kusini utoke nyikani kwa Sini, uendelee kando ya Edomu; hivyo mpaka wenu wa kusini utaanzia upande wa maawioni kwa jua kwenye mwisho wa Bahari ya Chumvi. Kisha huo mpaka upazungukie hapo pa kukwelea Akarabimu upande wake wa kusini, kisha upitie sini, utokee upande wa kusini wa Kadesi-Barnea, kisha utokee kwenye ua wa Adari na kufikia Asimoni. Kutoka Asimoni mpaka ukigeukie kijito cha Misri, upate kutokea baharini. Mpaka wenu wa upande wa baharini utakuwa Bahari Kubwa; huu utakuwa mpaka wenu wa upande wa baharini. Mpaka wenu wa kaskazini utoke kwenye Bahari Kubwa, mwufikishe mlimani kwa Hori; toka mlimani kwa Hori mwufikishe mpaka Hamati, kisha mpaka huu tokee Sedadi. Ukitoka hapo, mpaka uendelee kufika Zifuroni, kisha utokee kwenye ua wa Enani. Huu utakuwa mpaka wenu wa kaskazini. Mpaka wenu wa upande wa maawioni kwa jua utoke kwenye ua wa Enani, mwufikishe Sefamu; toka Sefamu mpaka na utelemkie Ribula na kupita Aini upande wa maawioni kwa jua; kisha mpaka uendelee kutelemka, hata ufike kando ya bahari ya Kinereti upande wake wa maawioni kwa jua. Kisha mpaka wa utelemke na kuufuata mto na Yordani, hata utokee kwenye Bahari ya Chumvi. Hii itakuwa nchi yenu yenye hiyo mipaka yake inayoizunguka pande zote. Kisha Mose akawaagiza wana wa Isiraeli kwamba: Hiyo ndiyo nchi, mtakayoipata kwa kupiga kura, mwichukue, iwe yenu, naye Bwana ameagiza kuipa yale mashina tisa na nusu ya Manase. Kwani wao wa shina la Rubeni wamekwisha kuipatia milango ya baba zao, nao wa shina la wana wa Gadi wamekwisha kuipatia milango ya baba zao, nao walio nusu ya shina la Manase wamekwisha kujipatia mafungu yao. Hayo mashina mawili na nusu ya shina la Manase wamekwisha kujipatia mafungu yao ng'ambo ya Yordani ya mashariki iliyo ya maawioni kwa jua, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili. Kisha Bwana akamwambia Mose kwamba: Haya ndiyo majina ya watu watakaowagawanyia ninyi nchi hiyo, iwe yenu: mtambikaji Elazari na Yosua, mwana wa Nuni. Tena sharti mchukue mkuu mmoja mmoja wa kila shina moja wa kusaidia kuigawanya nchi hiyo. Nayo haya ndiyo majina ya watu hao: wa shina la Yuda Kalebu, mwana wa Yefune. Wa shina la wana wa Simeoni Samueli, mwana wa Amihudi. Wa shina la Benyamini Elidadi, mwana wa Kisiloni. Wa shina la wana wa Dani mkuu Buki, mwana wa Yogli. Wa wana wa Yosefu: wa shina la wana wa Manase mkuu Hanieli, mwana wa Efodi. Wa shina la wana wa Efuraimu mkuu Kemueli, mwana wa Sifutani. Wa shina la wana wa Zebuluni mkuu Elisafani, mwana wa Parnaki. Wa shina la wana wa Isakari mkuu Paltieli, mwana wa Azani. Wa shina la wana wa Aseri mkuu Ahihudi, mwana wa Selomi. Wa shina la wana wa Nafutali mkuu Pedaheli, mwana wa Amihudi. Hawa ndio, Bwana aliowaagiza, kuwagawanyia wana wa Isiraeli mafungu yao katika nchi ya Kanaani. Kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili, Bwana akamwambia Mose kwamba: Waagize wana wa Isiraeli, wawape Walawi katika mafungu yao, watakayoyachukua, miji ya kukaa, nayo malisho yanayoizunguka hiyo miji mwape Walawi! Hiyo miji iwe yao ya kukaa, nayo malisho yawe ya ng'ombe wao na ya mbuzi na ya kondoo wao na ya nyama wao wengine wote. Hayo malisho ya miji, mtakayowapa Walawi, upana wao kutoka penye boma la mji kwenda nje sharti uwe mikono elfu kuuzunguka mji. Kwa hiyo na mpime huko nje ya mji upande wa maawioni kwa jua mikono 2000, nao upande wa kusini mikono 2000, nao upande wa baharini mikono 2000, nao upande wa kaskazini mikono 2000; nao mji uwe katikati; hayo na yawe malisho yao penye miji yao. Katika hiyo miji, mtakayowapa Walawi, sharti mwape miji sita ya kuikimbilia; hiyo mwape kwamba: mwuaji apate kuikimbilia. Pasipo kuihesabu hiyo mwape miji 42. Hivyo miji yote, mtakayowapa Walawi, itakuwa 48, ndiyo hiyo miji yenyewe pamoja na malisho yao. Mtakapoitoa hiyo miji katika mafungu, wana wa Isiraeli watakayoyachukua, yawe yao, kwao walio wengi na mtoe mingi, nako kwao walio wachache na mtoe michache; kila shina na litoe kwa ukuu wa fungu lake, litakalolipata kuwa lake, liwagawie Walawi miji ya kwao. Bwana akamwambia Mose kwamba: Sema na wana wa Isiraeli, uwaambie: Hapo, mtakapouvuka Yordani na kuingia katika nchi ya Kanaani, jichagulieni miji itakayowafalia ninyi kuwa miji ya kuikimbilia, mwuaji apate kuikimbilia, kama hakumpiga mwenziwe na kumwua kwa kusudi. Miji hiyo iwe kwenu ya kuikimbilia na kumkimbia mlipizi, mwuaji asife, mpaka asimamishwe mbele ya mkutano, ahukumiwe nao. Nayo miji, mtakayoitoa kuwa miji ya kuikimbilia, sharti iwe sita kwenu. Miji mitatu na mtoe ng'ambo ya huku ya Yordani, tena na mtoe miji mitatu katika nchi ya Kanaani, iwe miji ya kuikimbilia. Miji hiyo sita iwe ya kuikimbilia wana wa Isiraeli, nao wageni, nao watakaokaa kwao, wapate kuikimbilia wote wasioua mtu kwa kusudi. Lakini kama mtu amempiga mwenzake kwa chombo cha chuma, akafa, yule ni mwuaji, naye kwa kuwa ni mwuaji, hana budi kuuawa. Kama amempiga kwa jiwe, alilolishika, linaloweza kuua mtu, yule akafa, basi, ni mwuaji, naye kwa kuwa ni mwuaji, hana budi kuuawa. kama amempiga kwa chombo cha mti, alichokishika mkononi, kinachoweza kuua mtu, akafa, basi, ni mwuaji, naye kwa kuwa ni mwuaji, hana budi kuuawa. Mwenye kuilipiza hiyo damu na amwue mwuaji; hapo, atakapomkuta yeye, na amwue. Tena mtu akimkumba mwenzake kwa kumchukia, au akimtupia kitu kwa kumvizia, yule akafa, au akimpiga kwa mkono wake kwa uadui, yule akafa, basi, yule aliyempiga hana budi kuuawa, kwa kuwa ni mwuaji; naye mwenye kuilipiza hiyo damu na amwue huyo mwuaji hapo, atakapomkuta. Lakini kama amemkumba kwa mara moja tu pasipo kuvijua, isipokuwa kwa uadui, au kama amemtupia kitu cho chote pasipo kumvizia, au kama ameacha pasipo kumwona, jiwe lo lote linaloweza kumwua mtu limwangukie, naye yule akafa asipokuwa wala adui wake wala mwenye kumtakia baya, basi, wao wa mkutano watamwamulia yule aliyeua naye mwenye kuilipiza hiyo damu, wakiyafuata hayo maamuzi. Nao wa mkutano watamponya huyo aliyeua mikononi mwake mwenye kuilipiza hiyo damu, kisha wao wa mkutano na wamrudishe katika mji wa kuukimbilia, alimokimbilia, naye atakaa humo, mpaka atakapokufa mtambikaji mkuu, waliyempaka mafuta matakatifu. lakini kama yule mwuaji atatoka mipakani mwa mji wa kuukimbilia, alimokimbilia, naye mwenye kuilipiza hiyo damu akamwona nje ya mipaka ya huo mji, alimokimbilia, basi, mwenye kuilipiza hiyo damu atamwua huyo mwuaji pasipo kukora manza za damu. Kwani ilimpasa kukaa mle mjini, alimokimbilia, mpaka mtambikaji mkuu atakapokufa. Mtambikaji mkuu atakapokwisha kufa, huyo mwuaji naye atarudi kwao kwenye fungu lake, alilolichukua, liwe lake. Haya sharti yawe kwenu maongozi ya maamuzi ya vizazi vyenu po pote, mtakapokaa. Kila atakayemwua mwenziwe sharti wamwue huyo mwuaji kwa ushahidi wao walioviona, lakini shahidi mmoja asitoshe wa kuua mtu. Tena msichukue makombozi ya mtu mwuaji aliyekora manza za kufa, hana budi kuuawa. Wala msichukue makombozi ya mtu aliyekimbilia mji wa kuukimbilia, kwamba apate kurudi na kukaa kwao, mtambikaji akiwa hajafa bado. Wala msiipatie uchafu hiyo nchi, mtakayoiingia. Kwani damu huipatia nchi uchafu, tena haiwezekani kuipatia hiyo nchi upozi wa hiyo damu iliyomwagika kwake, isipokuwa kwa damu yake yeye aliyeimwaga hiyo damu. Kwa hiyo msiichafue hiyo nchi, ninyi mtakayoikaa, mimi nami nitakakokaa; kwani mimi Bwana nitakaa katikati ya wana wa Isiraeli. Wakuu wa milango ya ndugu za wana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, wa ndugu zao wana wa Yosefu, wakamkaribia Mose, wakasema mbele yake na mbele yao wakuu waliokuwa baba za milango ya wana wa Isiraeli, wakawaambia: Bwana amekuagiza wewe, bwana wetu, kuwapa wana wa Isiraeli nchi hiyo na kuwapigia kura, wapate mafungu ya nchi kuwa yao; nawe bwana wetu, umeagizwa na Bwana kuwapa wana wa kike wa ndugu yetu Selofuhadi fungu lake. Itakapotukia, mmoja miongoni mwa wana wa mashina mengine ya wana wa Isiraeli awaoe, ndipo, fungu lao litakapotoweka katika mafungu ya baba zetu, litiwe katika mafungu ya shina jingine litakalokuwa lao, wakiisha kuolewa; hivyo ndivyo, mafungu, tuliyoyapata kwa kupigiwa kura kuwa yetu, yatakavyopunguzwa. Nao mwaka wa shangwe utakapotimia kwa wana wa Isiraeli, fungu lao litatiwa vivyo hivyo katika mafungu ya shina jingine litakalokuwa lao kwa kuolewa kwao; ndivyo, hilo fungu lao litakavyotoweka katika mafungu ya shina la baba zetu. Ndipo, Mose alipowaagiza wana wa Isiraeli kwa kuagizwa na Bwana kwamba: Hayo, wao wa shina la wana wa Yosefu waliyoyasema, ni ya kweli. Hili ndilo neno, Bwana analowaagiza wana wa kike wa Selofuhadi kwamba: Mtu, watakayemwona kuwa mwema, wataolewa naye, lakini watakayeolewa naye sharti awe mtu wa ndugu za shina la baba yao. Ni kwa kwamba mafungu yao wana wa Isiraeli yasiondolewe katika shina moja na kutiwa katika shina jingine, ila wana wa Isiraeli sharti wagandamane kila mmoja na mafungu yaliyo ya shina la baba zao. Wana wa kike wote walio wenye fungu la nchi ya mashina ya wana wa Isiraeli sharti waolewe na mtu aliye wa ndugu za shina la baba yao, kusudi wana wa Isiraeli washike kila mmoja fungu lake la nchi, alilolipata kwa baba zake, liwe lake, kusudi mafungu ya nchi yasiondolewe katika shina moja na kutiwa katika shina jingine, ila mashina ya wana wa Isiraeli sharti wagandamane, kila mmoja akae katika fungu lake. Kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, wana wa kike wa Selofuhadi walivyofanya. Hao Mala, Tirsa na Hogla na Milka na Noa, wale wana wa kike wa Selofuhadi, wakaolewa na wana wa ndugu za baba yao. Wao waliookuwa ndugu zao wana wa Manase, mwana wa Yosefu, ndio waliolewa nao; kwa hiyo fungu lao likakaa kwake shina la ndugu za baba yao. Haya ndiyo maagizo na maamuzi, Bwana aliyowaagiza wana wa Isiraeli kinywani mwa Mose kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili. Haya ndiyo maneno, Mose aliyowaambia Waisiraeli wote ng'ambo ya huku ya Yordani nyikani kwenye mbuga zinazoielekea Bahari Nyekundu katikati ya Parani na Tofeli na Labani na Haseroti na Di-Dhahabu. Kutoka Horebu ulikuwa mwendo wa siku kumi na moja kwa kushika njia ya kwenda mlimani kwa Seiri mpaka Kadesi-Barnea. Ikawa siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na moja katika mwaka wa arobaini, ndipo, Mose alipowaambia wana wa Isiraeli hayo yote, kama Bwana alivyomwagiza kuwaambia. Ilikuwa hapo, alipokwisha kumpiga Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekaa Hesiboni, na Ogi, mfalme wa Basani, aliyekaa Astaroti karibu ya Edirei. Naye alikuwa ng'ambo ya huku ya Yordani katika nchi ya Moabu; ndiko, Mose alikoanza kuwaelezea mafunzo haya ya Maonyo, akasema: Bwana Mungu wetu alituambia kule Horebu kwamba: Siku za kukaa kwenu kwenye mlima huu zimetimia. Kwa hiyo ondokeni huku na kujielekeza kwenda milimani kwa Waamori nako kwao wote wanaokaa karibu yao nyikani na milimani na mabondeni na kusini na pwani kwenye bahari, mfike katika nchi ya Kanaani hata Libanoni mpaka ule mto mkubwa, lile jito la Furati. Tazameni, nchi hii iliyoko mbele yenu nitawapa, iingieni, mwichukue nchi hii, Bwana aliyowaapia baba zenu Aburahamu na Isaka na Yakobo kuwapa wao nao wa uzao wao watakaokuwapo nyuma yao. Hapo ndipo, nilipowaambia ninyi: Mimi peke yangu siwezi kuwatunza ninyi. Bwana Mungu wenu amewafanya kuwa wengi sana; nikiwatazam leo, mnafanana na nyota za mbinguni kwa wingi. Bwana Mungu wa baba zenu na aendelee kuwafanya kuwa wengi zaidi, wao walioko sasa waongezeke mara elfu, kisha na awabariki, kama alivyowaambia ninyi. Mimi nitawezaje peke yangu kuuchukua huo mzigo wenu mzito sana wa magomvi yenu? Kwa hiyo toeni kwenu watu werevu wa kweli walio watambuzi wanaojulikana katika mashina yenu, niwaweke kuwa vichwa vyenu. Nanyi mkanijibu kwamba: Neno hili, ulilolisema, linafaa kulifanya. Kisha nikiwachukua waliokuwa vichwa vya mashina yenu na watu waliojulikana kuwa wenye werevu wa kweli, nikawaweka kuwa vichwa vyenu, wawe wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia na wakuu wa hamsini na wakuu wa makumi, tena wawe wenye amri wa mashina yenu. Nao waamuzi wenu nikawaagiza siku hizo kwamba: Wasikilizeni ndugu zenu, mwamue kwa kweli, mtu akiwa na shauri la ndugu yake au la mgeni wake! Shaurini msiupendelee uso wa mtu, kama shauri lake ni dogo, au kama ni kubwa, wote mwasikilize pasipo kumwogopa ye yote, kwani hukumu ni yake Mungu. Lakini shauri likiwa gumu zaidi la kuwashinda ninyi, na mlilete kwangu, nilisikilize. Ndivyo, nilivyowaagiza siku zile mambo yote yaliyowapasa kuyafanya. Tulipoondoka Horebu tukasafiri katika ile nyika yote inayotisha kwa ukubwa wake, kama mlivyoona; tukaishika njia ya kwenda milimani kwa Waamori, kama Bwana Mungu wetu alivyotuagiza, tukafika mpaka Kadesi-Barnea. Ndipo, nilipowaambia: Mmefika milimani kwa Waamori, ndiyo nchi, Bwana Mungu wetu anayotaka kutupa sisi. Tazameni, Bwana Mungu wetu ameiweka nchi hii machoni penu. Pandeni tu kuichukua, iwe yenu, kama Bwana Mungu wa baba zenu alivyosema! Msiogope, wala msiingiwe na vituko! Ndipo, ninyi nyote mlipokuja kwangu, mkaniambia: Na tutume watu kwenda mbele yetu, watupelelezee nchi hii, kisha watuletee habari za njia, tutakazozishika za kupandia huko, na habari za miji, tutakayoiingia. Kwa kuwa neno hili lilikuwa jema machoni pangu, nikachagua kwenu watu kumi na wawili, kwa kila shina mtu mmoja. Wao wakajielekeza kupanda milimani, wakafika mpaka kijitoni kwa Eskoli wakiipeleleza nchi. Wakachukua kwa mikono yao matunda mengineyo ya nchi hiyo, wakashuka nayo kutuletea sisi, wakatuletea nazo habari za kwamba: Nchi hii, Bwana Mungu wetu anayotaka kutupa, ni nzuri. Lakini hamkutaka kupanda, mkalikataa agizo la Bwana Mungu wenu, mkanung'unika mahemani mwenu kwamba: Kwa kutuchukia Bwana alitutoa katika nchi ya Misri, atutie mikononi mwao Waamori, watuangamize. Sisi tupande kwenda wapi? ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu waliposema: Watu ni wengi na warefu kuliko sisi, nayo miji ni mikubwa yenye maboma yanayofika hata mbinguni; hata wana wa Anaki tumewaona huko. Ndipo, nilipowaambia ninyi: Msitetemeke, wala msiwaogope! Bwana Mungu wenu anayewatangulia, yeye atawapigia vita, matendo yake yawe kama yale yote, aliyowafanyizia kule Misri, mliyoyaona kwa macho yenu. Nako nyikani mmeona, Bwana Mungu wenu alivyowachukua, kama mtu anavyomchukua mwanawe, katika hizo safari zote, mlizokwenda, mpaka mkifika mahali hapa. Lakini ijapo ameyafanya hayo yote, ninyi hamkuwa mkimtegemea Bwana Mungu wenu. Naye alikuwa amewatangulia njiani, awatafutie mahali pa kupigia makambi yenu; aliwatangulia usiku kwa moto, awaangazie hizo njia, mlizokwenda, tena mchana kwa wingu. Hapo, Bwana alipoyasikia yale maneno, mliyoyasema, akachafuka, akaapa kwamba: Watu hawa wote wa hiki kizazi kibaya hawataiona kabisa hiyo nchi njema, niliyowaapia baba zao kuwapa, Kalebu, mwana wa Yefune, yeye tu ataiingia, nami nitampa nchi hiyo, aliyoikanyaga, iwe yake yeye na ya wanawe, kwa kuwa alimfuata Bwana kwa moyo wote. Mimi nami Bwana akanikasirikia kwa ajili yenu, akaniambia: Wewe nawe hutaiingia hiyo nchi. Lakini Yosua, mwana wa Nuni, anayekutumikia, yeye ataingia huko; mshikize moyo, kwani ndiye atakayewagawia Waisiraeli mafungu ya nchi yatakayokuwa yao. Nao watoto wenu, mliowasema, ya kama watakuwa mateka, nao wana wenu wasiojua leo bado kupambanua mema na mabaya, wao ndio watakaoingia huko, nao nitawapa hiyo nchi, waichukue, iwe yao. Lakini ninyi geukeni na kuondoka hapa, mrudi nyikani na kushika njia ya kwenda kwenye Bahari Nyekundu. Ndipo, mlipojibu na kuniambia: Tumemkosea Bwana. Sisi na tupande, tupige vita na kuyafanya yote, Bwana Mungu wetu aliyotuagiza. Lakini hapo mlipojifunga mata yenu ya kupigia vita kwa kuwaza, ya kama ni kazi nyepesi kupanda huko milimani, Bwana akaniambia: Waambie: Msipande, wala msipige vita! Kwani mimi simo katikati yenu, msije kupigwa mbele ya adui zenu. Nilipowaambia hayo, hamkusikia, mkalikataa neno, kinywa cha Bwana kililolisema; mkapanda milimani kwa kujivuna. Kwa hiyo Waamori waliokaa kule milimani walipotoka kupigana nanyi, wakawafukuza, kama nyuki wanavyofanya, wakawapiga ninyi huko Seiri, mfike mpaka Horma. Mkarudi na kumlilia Bwana, lakini Bwana hakuzisikia sauti zenu, wala hakuwategea ninyi sikio. Kwa hiyo mkakaa Kadesi hizo siku nyingi, mlizozikaa huko. Kisha tukageuka na kuondoka huko, turudi nyikani na kushika nja ya kwenda kwenye Bahari Nyekundu, kama Bwana alivyoniambia, tukazunguka siku nyingi kwenye mlima wa Seiri. Kisha Bwana akaniambia kwamba: Siku, mlizouzunguka mlima huu, ni nyingi, sasa geukeni kwenda upande wa kaskazini! Waagize watu kwamba: Piteni katika mipaka yao ndugu zenu wana wa Esau wanaokaa Seiri! Wao watawaogopa ninyi, lakini jiangalieni sana, msiwapelekee vita! Kwani sitawapa ninyi hata kipande kidogo cha nchi yao, ijapo pawe pa kukanyagia kwa mguu mmoja tu, kwani mlima wa Seiri nilimpa Esau, auchukue, uwe nchi yake. Chakula sharti mjinunulie kwao kwa fedha, mpate kula, nayo maji ya kunywa sharti myanunue kwao kwa fedha. Kwani Bwana Mungu wako amekubariki katika mambo yote, uliyoyafanya kwa mkono wako, anazijua safari zako, ulizozifanya katika nyika hii kubwa; hii miaka arobaini Bwana Mungu wako amekuwa pamoja na wewe, usikose cho chote. Ndipo, tulipoendelea kusafiri na kuondoka kwao ndugu zetu wana wa Esau waliokaa Seiri, tukaziacha njia za huko nyikani na za Elati na za Esioni-Geberi, tukageuka na kushika njia ya kwenda kwenye nyika ya Moabu. Ndipo, Bwana aliponiambia: Usiwasonge Wamoabu, wala msiwapelekee vita mkipigana nao! Kwani sitakupa kipande cha nchi yao, mwichukue, iwe yenu, kwa kuwa naliwapa wana wa Loti nchi ya Ari, waichukue, iwe yao. Kale Waemi walikaa huko, nao walikuwa watu wakubwa na warefu wengi mno kama Waanaki. Nao waliwaziwa kuwa Majitu kama Waanaki, lakini Wamoabu waliwaita Waemi. Huko Seiri kale walikaa Wahori; ndio, wana wa Esau waliowafukuza na kuwaangamiza mbele yao, kisha wakakaa mahali pao, kama Waisiraeli walivyofanya katika nchi, waliyoichukua, iwe yao, Bwana aliyowapa. Sasa inukeni, mkivuke kijito cha Zeredi! Ndipo, tulipokivuka hicho kijito cha Zeredi. Nazo siku, tulizosafiri toka Kadesi-Barnea mpaka tulipokivuka kijito cha Zeredi, zilikuwa miaka 38; ndipo, kile kizazi chote cha wapiga vita kilipokuwa kimeishilizwa makambini, kama Bwana alivyowaapia. Nao mkono wa Bwana ulikuwa ukiwapingia, upate kuwaangamiza makambini, mpaka waishilizwe kabisa. Ikawa, wale wapiga vita walipokwisha kuishilizwa wote na kuondolewa kwa wenzao wa ukoo kwa hivyo, walivyokufa, Bwana akaniambia kwamba: Leo hivi wewe upite mpaka wa Moabu na kupita Ari. Kisha utafika karibu kwao wana wa Amoni; usiwasonge, wala usiwapelekee vita! Kwani sitakupa kipande cha nchi ya wana wa Amoni, ukichukue, kiwe chako, kwani nchi hiyo naliwapa wana wa Loti, waichukue, iwe yao. Nchi hii nayo iliwaziwa kuwa ya Majitu; kale Majitu walikaa huko kweli, nao Waamoni waliwaita Wazamuzumi. Nao walikuwa watu wakubwa na warefu wengi mno kama Waanaki, lakini Bwana aliwaangamiza mbele yao; ndipo, walipoichukua nchi yao, iwe yao, wakakaa mahali pao. Ni vivyo hivyo, alivyowafanyizia wana wa Esau wanaokaa Seiri, maana mbele yao waliwaangamiza Wahori, wapate kuichukua nchi yao na kukaa huko mahali pao mpaka siku hii ya leo. Nao Waawi waliokaa vijijini mpaka Gaza waliangamizwa na Wakafutori waliotoka Kafutori, kisha wao walikaa mahali pao. Nanyi inukeni na kuondoka huku, mkivuke kijito cha Arnoni! Tazama Mwamori Sihoni, mfalme wa Hesiboni, nimemtia mikononi mwako pamoa na nchi yake. Haya! Anza kuichukua ukimpelekea vita, upigane naye! Leo hivi nitaanza kuyatisha makabila yote chini ya mbingu, wakustukie kwa kukuogopa; watakapousikia uvumi wako watakutetemekea na kujipinda kwa machungu. Ndipo, nilipotuma wajumbe toka nyikani kwa Kedemoti kwake Sihoni, mfalme wa Hesiboni, kumwambia maneno haya ya mapatano kwamba: Ninataka kupita katika nchi yako na kwenda njiani tu, nisiondoke njiani kwenda wala kuumeni wala kushotoni. Chakula utaniuzia kwa fedha, nipate kula, nayo maji utanipa kwa fedha, nipate kunywa ninataka kupita tu kwa miguu yangu. Hivyo ndivyo, walivyonifanyizia nao wana wa Esau wanaokaa Seiri, nao Wamoabu wanaokaa Ari; fanya hivyo nawe, mpaka nitakapouvuka Yordani, niingie nchi, Bwana Mungu wetu aliyotupa. Lakini Sihoni, mfalme wa Hesiboni, hakutaka kutupa ruhusa ya kupita kwake, kwa kuwa Bwana Mungu wako alimpa mawazo magumu rohoni na kuushupaza moyo wake, apate kumtia mikononi mwako, kama inavyoelekea sasa. Ndipo, Bwana aliponiambia: Tazama, nimeanza kumtoa Sihoni na nchi yake mbele yako. Nawe anza kuichukua nchi yake, iwe yako! Sihoni alipotoka asubuhi, yeye pamoja na watu wake wote, wapigane nasi kule Yasa, Bwana Mungu wetu akamtoa mbele yetu, tukampiga, yeye na wanawe na watu wake wote, tukaiteka miji yake yote siku hizo, tukawatia mwiko wa kuwapo wote pia waliokuwamo mijini, wanawaume na wanawake na watoto, hatukusaza hata mmoja aliyeweza kukimbia. Ni nyama tu wa kufuga na nyara za miji, tuliyoiteka, ndizo tulizojichukulia. Toka Aroeri ulioko ukingoni kwenye kijito cha Arnoni, katika miji iliyoko kule kwenye kijito mpaka Gileadi haukuwako mji wenye boma refu la kutushinda, yote pia Bwana Mungu wetu aliitoa mbele yetu. Nchi ya wana wa Amoni tu hukuikaribia, ile nchi yote iliyoko kando ya kijito cha Yakobo pamoja na miji ya milimani; kwani hiyo yote Bwana Mungu wetu alitukataza kuichukua. Kisha tukageuka, tukapanda na kushika njia ya Basani. Naye Ogi, mfalme wa Basani, akatoka, atujie yeye pamoja na watu wake wote, wapigane nasi kule Edirei. Lakini Bwana akaniambia: Usimwogope! Kwani nimemtia mikononi mwako pamoja na watu wake wote na nchi yake. Nawe umfanyizie, kama ulivyomfanyizia Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekaa Hesiboni. Kisha Bwana Mungu wetu akamtia mikononi mwetu huyo Ogi, mfalme wa Basani, pamoja na watu wake wote, tukampiga, hatukusaza kwake hata mmoja aliyeweza kukimbia. Tukaiteka miji yake yote siku hizo, haukuwako mji kwao, tusiouchukua: miji 60 nacho hicho kipande kizima cha Argobu, ndio ufalme wote wa Ogiwa Basani. Miji hiyo yote ilikuwa yenye maboma magumu na marefu na malango na makomeo; tena tukapata miji mingi sana iliyokuwa wazi. Tukawatia mwiko wa kuwapo, kama tulivyomfanyizia Sihoni, mfalme wa Hesiboni, tulipowatia mwiko wa kuwapo wote pia waliokuwamo mijini, wanawaume na wanawake na watoto. Lakini nyama wa kufuga wote na nyara za miji tukajichukulia. Ndivyo, tulivyozichukua siku hizo nchi za wafalme wawili wa Waamori waliokaa ng'ambo ya huku ya Yordani toka kijito cha Arnoni mpaka milimani kwa Hermoni. Wasidoni waliita milima ya Hermoni Sirioni, nao Waamori waliiita Seniri. Nasi tukaichukua miji yote ya nchi ya tambarare na nchi yote ya Gileadi na ya Basani mpaka Salka na Edirei, iliyokuwa miji ya ufalme wa Ogi kule Basani. Yeye ogi, mfalme wa Basani, alikuwa amesalia peke yake kwa masao ya Majitu; mkikitazama kitanda chake, ni kitanda cha chuma, nacho kingaliko katika mji wa Raba wa wana wa Amoni, urefu wake ni mikono tisa, nao upana wake ni mikoni minne, mkipima kwa mikono wa mtu. Siku hizo tukaichukua nchi hiyo, iwe yetu toka Aroeri ulioko kwenye kijito cha Arnoni. Nusu ya milima ya Gileadi pamoja na miji yake ikawapa Warubeni na Wagadi. Kipande cha Gileadi kilichosalia na Basani yote iliyokuwa ufalme wa Ogi nikawapa wao wa nusu ya shina la Manase, ni kipande chote cha Argobu pamoja na Basani yote inayoitwa nchi ya Majitu. Yairi, mwana wa Manase, alikichukua kile kipande chote cha Argobu hata mpakani kwa Wagesuri na Wamakati, akaziita hizo nchi za Basani kwa jina lake Mahema ya Yairi; ndivyo, zinavyoitwa hata leo. Makiri nikampa Gileadi. Warubeni na Wagadi nikawapa kipande cha Gileadi mpaka kijito cha Arnoni, mpaka uwe mtoni katikati; tena mpaka ukafika kijito cha Yakobo ulio mpaka wa wana wa Amoni. Tena nyika inayopakana na Yordani toka Kinereti hata kwenye bahari ya nyikani, ndio Bahari ya Chumvi chini ya matelemko ya Pisiga upande wa maawioni kwa jua. Siku hizo nikawagiza ninyi kwamba: Bwana Mungu wenu amewapa nchi hii, mwichukue, iwe yenu; kwa hiyo wa kwenu wote walio wenye nguvu na washike mata ya vita, mvuke mbele ya ndugu zenu hao wana wa Isiraeli. Wanawake na watoto wenu na makundi yenu tu na wakae katika miji yenu, kwani najua, ya kuwa mnayo makundi mengi. Hapo, Bwana atakapowapatia ndugu zenu kutulia kama ninyi, nao watakapokwisha kuichukua nchi, Bwana Mungu wenu atakayowapa ng'ambo ya huko ya Yordani, ndipo, mtakaporudi kila mtu kwenye nchi yake, aliyoichukua, iwe yake, niliyowapa ninyi. Naye Yosua nikamwagiza siku hizo kwamba: Macho yako yameyaona yote, Bwama Mungu wetu aliyowafanyizia hao wafalme wawili; hivyo ndivyo, Bwana atakavyozifanyizia nchi zote za kifalme, utakazoziingia wewe. Msiwaogope! Kwani Bwana Mungu wenu ndiye atakayewapigia vita. Siku hizo nikambembeleza Bwana kwamba: Bwana Mungu wangu, wewe umeanza kumwonyesha mtumishi wako ukuu wako na nguvu za mkono wako; kwani yuko Mungu gani mbinguni na duniani anayeweza kufanya matendo, kama hayo ya uwezo wako mwingi? Nipe ruhusa, nivuke, niione nchi hiyo njema iliyoko ng'ambo ya Yordani, hiyo milima mizuri, nayo ya Libanoni. Lakini Bwana alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, kwa hiyo Bwana hakunisika, akaniambia: Acha tu! Usiseme tena na mimi kwa ajili ya shauri hili! Panda juu mlimani kwa Pisiga, uyainue macho yako na kuyaelekeza upande wa baharini na wa kaskazini na wa kusini na wa maawioni kwa jua, uitazame hiyo nchi kwa macho yako. Kwani hutauvuka mto huu wa Yordani. Mwagizie Yosua mambo yako! Mtie nguvu na kumshikiza moyo! Kwani yeye ndiye atakayevuka mbele ya watu hawa, naye ndiye atakayewagawia nchi hiyo, utakayoiona, iwe yao. Kisha tukakaa bondeni na kuelekea Beti-Peori. Sasa Isiraeli, yasikilize maongozi na maamuzi, nitakayowafundisha, myafanye, mpate kupona na kuiingia na kuichukua hiyo nchi, Bwana Mungu wa baba zenu atakayowapa, iwe yenu. Hayo, mimi nitakayowaagiza, msiyaongeze, wala msiyapunguze, ila yaangalieni haya maagizo ya Bwana Mungu, mimi nitakayowaagiza ninyi! Macho yenu yameyaona, Bwana aliyomfanyizia Baali-Peori, kwani wao wote waliomfuata Baali-Peori amewaangamiza Bwana Mungu wako, watoweke kwako. Lakini ninyi mliogandamana na Bwana Mungu wenu mnaishi nyote hata leo. Tazameni, nimewafundisha ninyi maongozi na maamuzi, kama Bwana Mungu wangu alivyoniagiza; yafanyeni yayo hayo katika nchi hiyo, mtakayoiingia kuichukua, iwe yenu. Yaangalieni, myafanye! Kwani huo utakuwa werevu wenu wa kweli na utambuzi wenu machoni pao yale makabila watakayoyasikia hayo maongozi yenu yote, waseme; Kumbe watu hawa ni werevu wa kweli na watambuzi, kwa hiyo ni kabila kubwa. Kwani liko taifa gani kubwa, miungu yake inalolikalia karibu hivi, kama Bwana Mungu wetu alivyo karibu kwetu po pote, tunapomlilia? Tena liko taifa gani kubwa lililo lenye maongozi na maamuzi yaongokayo kama haya maonyo yote, mimi ninayowatolea ninyi leo masikioni penu? Jiangalie tu na kuiangalia roho yako, usiyasahau kabisa hayo mambo, macho yako yaliyoyaona, yasiondoke moyoni mwako siku zote, utakazokuwapo. Nawe uyajulishe kwa wanao na kwa wana wa wanao! Wakumbushe mambo ya siku ile, uliposimama mbele ya Bwana Mungu wako kule Horebu, Bwana aliponiambia: Kusanya kwangu watu hawa, niseme maneno yangu masikioni mwao, wajifunze kunicha siku zote, watakazokuwapo katika nchi, kisha wawafundishe wana wao nao. Napo, mlipomkaribia na kusimama mlimani chini, mlima ukawaka moto mpaka juu ndani ya mbinguni, kukawa na giza na mawingu meusi kabisa. Ndipo, Bwana aliposema nanyi toka motoni, nanyi mkazisikia sauti za maneno yake, lakini hakuna mwenye mwili, mliyemwona, ni kuzisikia hizo sauti tu. Ndivyo, alivyowatangazia Agano lake, alilowaagiza kulifanya, yale maagizo kumi, kisha akayaandika katika mbao mbili za mawe. Mimi nami Bwana akaniagiza siku hizo kuwafundisha maongozi na maamuzi, myafanye katika hiyo nchi, mnayotaka kuivukia, mwichukue, iwe yenu. Ziangalieni sana roho zenu! Kwani hamkuona mwenye mwili ye yote siku hiyo, Bwana aliposema nanyi kule Horebu toka motoni. Msijiponze na kujifanyizia kinyago cho chote cha kuchongwa, wala cha kuyeyushwa, wala cha kuchorwa maweni kwa mfano wa mtu mume au mke, wala kwa mfano wo wote wa nyama wa huku nchini, wala kwa mfano wo wote wa ndege mwenye mabawa ya kurukia angani, wala kwa mfano wo wote wa dudu atambaaye mchangani, wala kwa mfano wo wote wa samaki wa majini chini ya nchi! Wala usiyainue macho yako na kuyaelekeza mbinguni, ulitazame jua na mwezi na nyota, hivyo vikosi vya mbinguni, usijaribiwe kuviangukia na kuvitumikia, kwa kuwa Bwana Mungu wako aliviwekea makabila yote pia yaliyoko chini ya mbingu yote nzima. Lakini ninyi Bwana aliwachukua na kuwatoa katika tanuru ya kuyeyushia vyuma, ndio Misri, mwe kabila llilo lake yeye mwenyewe, kama inavyoelekea leo. Kisha Bwana akanikasiria mimi kwa ajili yenu, akaapa, kwamba nisiuvuke Yordani, nisiingie hiyo nchi njema, Bwana Mungu wako atakayokupa wewe, iwe fungu lako mwenyewe. Kwa hiyo mimi nitakufa katika nchi hii pasipo kuuvuka Yordani; lakini ninyi mtauvuka, mwichukue hiyo nchi njema, iwe yenu. Jiangalieni, msilisahau Agano la Bwana Mungu wenu, alilolifanya nanyi, msijifanyizie kinyago cho chote cha kuchongwa, wala cha kuyeyushwa kwa mfano wo wote, Bwana Mungu wako aliokukataza. Kwani Bwana Mungu wako ni moto ulao, yeye ni Mungu mwenye wivu. Mtakapozaa wana na wana wa wana, mwe wazee katika nchi hiyo, msijiponze na kujifanyizia kinyago cho chote cha kuchongwa, wala cha kuyeyushwa, kwani hivyo mtafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana Mungu wenu, mmkasirishe. Kwa hiyo nazitaja mbingu na nchi, ziwashuhudie leo hivi, ya kama hivyo mtaangamia upesi na kutoweka katika nchi hiyo, mnayovukia Yordani, mje kuichukua, iwe yenu, hamtakaa siku nyingi ndani yake, ila mtaangamizwa kabisa. Yeye Bwana atawatawanya katika makabila mengine, msalie wachache wanaohesabika upesi kwao wamizimu, Bwana atakakowapeleka. Huko ndiko, mtakakotumikia miungu iliyo kazi za mikono ya watu, iliyo miti na mawe, isiyoona, isiyosikia, isiyokula, isiyonusa. Lakini mtakapomtafuta huko Bwana Mungu wenu mtamwona, ukimtafuta kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote. Utakaposongeka kwa kupatwa na mambo hayo yote siku zile za mwisho, ndipo, utakaporudi kwa Bwana Mungu wako, uzisikilize sauti zake. Kwani Bwama Mungu wako ni Mungu mwenye huruma, hatakuacha kabisa, wala hatakuangamiza kabisa, wala hatalisahau Agano, alilowaapia baba zako. Uliza tu mambo ya siku za kale zilizokuwa mbele yako tangu siku ile, Mungu alipomwumba Adamu na kumweka katika nchi, tena chunguza tangu mwisho wa huku wa mbingu hata mwisho wa huko wa mbingu, kama lilifanyika, au kama lilisikilika jambo kubwa kama hili. Wako watu walioisikia sauti ya Mungu, akisema toka motoni, kama wewe ulivyoisikia, kisha wawepo wenye uzima? Au Mungu alijaribu hata penginepo kuja kujichukulia taifa moja katikati ya mataifa mengine kwa majaribu na kwa vielekezo na kwa vioja na kwa kupiga vita na kwa kutoa nguvu za kiganja chake na kwa kuukunjua mkono wake na kwa matisho makuu yanayoogopesha, kama Bwana Mungu wenu alivyowafanyizia ninyi kule Misri machoni pako? Wewe ulionyeshwa hayo, upate kujua, ya kuwa Bwana ni Mungu, hakuna mwingine tena, asipokuwa yeye peke yake. Uliisikia sauti yake, ikitoka mbinguni, ipate kukuonya, nako huku nchini alikuonyesha moto wake mkubwa, nako kutoka humo motoni ukaisikia sauti yake. Kwa kuwa aliwapenda baba zako, akawachagua halafu wao wa uzao wao, akakutoa Misri kwa nguvu zake kuu akikuongoza kwa uso wake, afukuze mbele yako mataifa makubwa yenye nguvu za kukushinda wewe, akuingize kwao na kukupa nchi yao, iwe yako, kama inavyoelekea leo. siku hii ya leo yajue na kuyaweka moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu mbinguni juu na huku nchini chini, hakuna mwingine tena. Kwa hiyo yaangalieni maongozi yake na maagizo yake, mimi ninayokuagiza leo, upate kuona mema wewe na wanao watakaokuwapo nyuma yako, siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi, akupayo Bwana Mungu wako, iwe yako siku zote. Kisha Mose akatenga miji mitatu ng'ambo ya Yordani ya maawioni kwa jua, mtu apate kuikimbilia, kama amemwua mwenziwe pasipo kujua, naye alipokuwa si mchukivu wake tangu zamani, basi, atakapokimbilia mmojawapo hiyo miji, awe amepona. Nayo ni hii: Beseri wa nyikani katika nchi ya tambarare kwa Warubeni na Ramoti wa Gileadi kwa Wagadi na Golani wa Basani kwa Wamanase. Haya ndiyo maonyo, Mose aliyowawekea wana wa Isiraeli; tena ndiyo mashuhuda na maongozi na maamuzi, Mose aliyowaambia wana wa Isiraeli, walipotoka Misri. Aliyasema ng'ambo ya huku ya Yordani katika bonde linaloelekea Beti-Peori katika nchi ya Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekaa Hesiboni, Mose na wana wa Isiraeli waliyempiga walipotoka Misri. Nayo nchi yake wakaichukua, iwe yao, hata nchi ya Ogi, mfalme wa Basani; hawa wafalme wawili wa Waamori ndio waliokaa ng'ambo ya Yordani ya maawioni kwa jua, toka Aroeri ulioko ukingoni kwenye kijito cha Arnoni mpaka milimani kwa Sioni, ndio Hermoni, nayo nyika yote ya ng'ambo ya Yordani ya maawioni kwa jua mpaka kwenye bahari ya nyikani chini ya matelemko ya Pisiga. Mose akawapazia sauti Waisiraeli wote, akawaambia: Sikieni, Waisiraeli, maongozi na maamuzi, mimi ninayoyasema leo masikioni mwenu, mjifundishe na kuyaangalia, mpate kuyafanya! Bwana Mungu wetu alifanya Agano na sisi kule Horebu; Agano hilo Bwana hakulifanya na baba zetu, ila na sisi wenyewe tuliopo leo hapa sote wenye uzima. Huko mlimani Bwana alisema nasi uso kwa uso toka motoni. Siku hiyo mimi nilisimama katikati ya Bwana nanyi, niwatangazie Neno la Bwana, kwani mliuogopa ule moto, kwa hiyo hamkupanda mlimani; naye alisema: Mimi ndimi Bwana Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi! Usijifanyie kinyago, wala mfano wo wote wa vitu vilivyoko mbinguni juu, wala vilivyoko nchini chini, wala vilivyomo majini chini ya nchi! Usivitambikie, wala usivitumikie! Kwani mimi Bwana Mungu wako ni Mungu mwenye wivu; manza za baba nitazipatilizia wana, nikifikishe kizazi cha tatu na cha nne, kwao wanichukiao. Lakini nitawafanyizia mema, nikifikishe hata kizazi cha maelfu, kwao wanipendao na kuyashika maagizo yangu. Usilitaje Jina la Bwana Mungu wako bure! Kwani Bwana hatamwachilia alitajaye Jina lake bure. Ishike siku ya mapumziko kuitakasa, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza! Siku sita sharti ufanye kazi, uyamalize mambo yako yote! Lakini siku ya saba ndiyo ya kumpumzikia Bwana Mungu wako. Hapo usifanye kazi yo yote, wala wewe, wala mwanao wa kiume, wala wa kike, wala mtumishi wako wa kiume, wala wa kike, wala ng'ombe wako wala punda wako wala nyama wako ye yote wa kufuga, wala mgeni wako aliomo malangoni mwako, mtumishi wako wa kiume na wa kike apate kupumzika kama wewe! Sharti ukumbuke, ya kama ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, naye Bwana Mungu wako akakutoa huko kwa kutoa nguvu za kiganja chake na kwa kuukunjua mkono wake; kwa hiyo Bwana Mungu wako alikuagiza kuifanya siku ya mapumziko. Mheshimu baba yako na mama yako, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza, siku zako zipate kuwa nyingi, nawe upate kuona mema katika nchi, akupayo Bwana Mungu wako! Usiue! Usizini! Usiibe! Usimshuhudie mwenzio uwongo! Usimtamani mke wa mwenzio! Wala usiitamani nyumba ya mwenzio, wala shamba lake, wala mtumishi wake wa kiume, wala wa kike, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote, mwenzio alicho nacho! Maneno haya Bwana aliwaambia wao wote wa mkutano wenu kule mlimani kwa sauti kuu toka motoni mle winguni mwenye weusi, hakuongeza neno, kisha akayaandika katika mbao mbili za mawe, akanipa mimi. Ikawa, mlipoisikia sauti toka gizani, nao mlima ulipowaka moto, mkanikaribia ninyi mliokuwa vichwa vya mashina yenu na wazee wenu, mkasema: Tazama, Bwana Mungu wetu ametuonyesha utukufu na ukuu wake, tukaisikia nayo sauti yake toka motoni, siku hii ya leo tumeona, ya kuwa Bwana anasema na mtu, naye hafi. Sasa mbona tufe, moto huu mkubwa ukitula? Tukiendelea kuisikia tena sauti ya Bwana Mungu wetu hatuna budi kufa. Kwani yuko wapi mwingine mwenye mwili, ndiye aisikie kama sisi sauti ya Mungu Mwenye uzima, akisema toka motoni, kisha awepo mwenye uzima? Nenda wewe, uyasikilize yote, Bwana Mungu wetu atakayoyasema, kisha wewe tuambie yote, Bwama Mungu wetu aliyoyasema! Nasi tutakapoyasikia tutayafanya. Bwana alipozisikia sauti za maneno yenu, mliyoniambia, yeye Bwana akaniambia: Nimezisikia sauti za maneno ya watu hawa, waliyokuambia, hayo yote waliyoyasema ni mema. Laiti wangekuwa siku zote wenye mioyo inayoniogopa hivyo, wayaangalie maagizo yangu yote, wao na wana wao wapate kuona mema kale na kale! Nenda, uwaambie: Rudini tu mahemani mwenu! Lakini wewe uje hapa kusimama kwangu, nikuambie maagizo na maongozi na maamuzi yote, utakayowafundisha, wayafanye katika nchi hiyo, mimi nitakayowapa, waichukue, iwe yao. Kwa hiyo angalieni, mfanye, kama Bwana Mungu wenu alivyowaagiza ninyi, msiondoke kwake kwenda wala kuumeni wala kushotoni! Ila njia zote, Bwana Mungu wenu alizowaagiza ninyi, zishikeni na kuzifuata, mkae uzimani na kuona mema, nazo siku zenu ziwe nyingi katika nchi, mnayokwenda kuichukua, iwe yenu. Nayo haya ndiyo maagizo na maongozi na maamuzi, Bwana Mungu wenu aliyoniagiza, niwafundishe ninyi, mpate kuyafanya katika nchi, mnayoivukia kuichukua, iwe yenu. Sharti umwogope Bwana Mungu wako, uyaangalie maongozi na maagizo yake yote, ninayokuagiza, wewe na wanao na wana wa wanao siku zote za maisha yako, kusudi siku zako zipate kuwa nyingi. Isiraeli, yasikie na kuyaangalia, uyafanye, kusudi uone mema, nanyi mpate kuwa wengi sana, kama Bwana Mungu wa baba zako alivyokuagia kukupa nchi ichuruzikayo maziwa na asali. *Sikia, Isiraeli: Bwana Mungu wetu ni Bwana peke yake. Nawe umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa nguvu yako yote. Maneno haya, ninayokuagiza leo, sharti yawe moyoni mwako. Jikaze kuwafundisha watoto wako na kuyasema nao ukikaa nyumbani mwako, ukienda safari zako, ukitaka kulala, hata ukiamka! Yafunge mkononi pako kuwa kielekezo, yawe napo pajini pako katikati ya macho yako! Yaandike vizingitini namo milangoni nyumbani mwako! Hapo Bwana Mungu wako atakapokuingiza katika hiyo nchi, aliyowaapia baba zako Aburahamu na Isaka na Yakobo, kwamba akupe wewe miji mikubwa mizuri, usiyoijenga, na nyumba zijaazo mema yote, usizozijaza, na visima vilivyochimbuliwa, usivyovichimbua, na mizabibu na michekele, usiyoipanda, basi, hapo utakapoila na kushiba, jiangalie, usimsahau Bwana aliyekutoa katika nchi ya Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa! Mwogope Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye! Hapo utakapoapa litaje Jina lake!* Msifuate miungu mingine miongoni mwa miungu ya makabila yanayowazunguka! Kwani Bwana Mungu wako anayekaa katikati yako ni Mungu mwenye wivu; angalia, makali yake Bwana Mungu wako yasikuwakie, akakuangamiza, utoweke juu ya nchi. Msimjaribu Bwana Mungu wenu, kama mlivyomjaribu kule Masa. Yaangalieni sana maagizo ya Bwana Mungu wenu na mashuhuda yake na maongozi yake, aliyoyaagiza! Yafanye yaongokayo nayo yafaayo machoni pake Bwana, kusudi uone mema, upate kuingia katika hiyo nchi njema, Bwana aliyowaapia baba zako, uichukue, iwe yako. Naye na akupe kuwakimbiza adui zako wote mbele yako, kama Bwana alivyosema. Mwanao atakapokuuliza siku zijazo kesho kwamba: Nini maana yao haya mashuhuda na maongozi na maamuzi, Bwana Mungu wetu aliyowaagiza ninyi? ndipo umwambie mwanao: Sisi tulikuwa watumwa wa Farao kule Misri, lakini Bwana akatutoa Misri kwa mkono wake wenye nguvu, Bwana alipofanya machoni petu kule Misri vielekezo na vioja vikubwa vilivyomwogopesha Farao na mlango wake wote. Ndivyo, alivyotutoa huko na kutuleta huku, atupe nchi hii, aliyowaapia baba zenu. Ndipo, Bwana alipotuagiza kuyafanya haya maongozi yote kwa kumcha Bwana Mungu wetu, tuone mema siku zote za maisha yetu, kama inavyoelekea leo. Nao wongofu wetu ndio huu wa kujiangalia, tuyafanye haya maagizo yote mbele ya Bwana Mungu wetu, kama alivyotuagiza. Bwana Mungu wako atakapokuingiza katika nchi hiyo, utakayoiingia kuichukua, iwe yako, ndpo, atakapong'oa huko mbele yako mataifa mengi, Wahiti na Wagirgasi na Waamori na Wakanaani na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi, ndio mataifa saba yaliyo yenye watu wengi na yenye nguvu kuliko wewe. Bwana Mungu wako atakapowatoa mbele yako, uwapige, sharti uwatie mwiko kabisa wa kuwapo, usifanye agano nao, wala usiwahurumie. Wala usioane nao: mwanao wa kike usimpe mwana wa kiume wa kwao, wala mwana wa kike wa kwao usimpe mwanao wa kiume. Kwani ataugeuza moyo wa mwanao, aache kunifuata, watumikie miungu mingine; ndipo, makali ya Bwana yatakapokuwakia, akuangamize upesi. Ila mwafanyizie hivyo: pao pa kutambikia sharti mpabomoe, nazo nguzo zao za mawe za kutambikia mzivunje, nayo miti yao ya Ashera mwikate, navyo vinyago vyao vya kuchongwa mviteketeze kwa moto. Kwani wewe ndiwe kabila takatifu la Bwana Mungu wako; wewe Bwana Mungu wako alikuchagua katika makabila yote yaliyoko huku nchini, uwe kabila lake mwenyewe. Bwana hakushikamana nanyi na kuwachagua, kwa kuwa m wengi kuliko makabila mengine, kwani mlikuwa wachache kuliko makabila yote, ila kwa kuwa Bwana aliwapenda ninyi, akataka kukitimiza kiapo, alichowaapia baba zenu, kwa hiyo Bwana aliwatoa ninyi kwa mkono wake wenye nguvu, akawakomboa mkononi mwa Farao, mfalme wa Misri, na kuwatoa nyumbani, mlimokuwa watumwa. Kwa hiyo jua, ya kuwa Bwana Mungu wako ni Mungu kweli, ni Mungu mwelekevu anayeyatimiza maagano na magawio kwao wampendao na kuyashika maagizo yake, akifikishe hata kizazi cha maelfu. Lakini wao wamchukiao huwalipisha waziwazi na kuwaangamiza, hakawii kumlipisha waziwazi amchukiaye. Kwa hiyo yaangalieni maagizo na maongozi na maamuzi, mimi ninayokuagiza leo kuyafanya. Itakuwa, mtakapoyasikia haya maamuzi na kuyaangalia, myafanye, naye Bwana Mungu wako atakutimilizia maagano na magawio, aliyowaapia baba zako. Ndipo, atakapokupenda, akubariki na kukufanya kuwa wengi, ayabariki nayo mazao ya tumbo lako nayo mazao ya shamba lako, ngano zako na mvinyo zako mbichi na mafuta yako na ndama wako na wana kondoo wako, watakaozaliwa katika nchi hiyo, Bwana aliyowaapia baba zako kukupa. Utakuwa umebarikiwa kuliko makabila yote, hatakuwa kwako mtu, wala mume, wala mke asiyezaa, nao nyama wenu wa kufuga watakuwa vivyo hivyo. Nao ugonjwa wote Bwana atauondoa kwako, hata hayo maradhi mabaya ya Misri, unayoyajua, atayazuia kwako, atayafikisha tu kwao wote wakuchukiao. Nayo makabila yote, Bwana Mungu wako atakayokupa, uyale, usiyaonee huruma kabisa, wala usiitumikie miungu yao, kwani hii itakuwa tanzi la kukunasa. Napo, utakaposema moyoni mwako: Mataifa haya ni mengi ya kunishinda, nitawezaje kuyafukuza? Usiwaogope, ila yakumbuke sana, Bwana Mungu wako aliyomfanyizia Farao nao Wamisri wote. Yakumbuke hayo majaribu makuu, macho yako yaliyoyaona, navyo vielekezo na vioja, nacho kiganja chake chenye nguvu, nao mkono, Bwana Mungu wako alioukunjua alipokutoa. Hivyo ndivyo, Bwana Mungu wako atakavyoyafanyizia makabila yote, wewe unayoyaogopa. Tena Bwana Mungu wako atatuma mavu kwao, waangamie nao watakaosalia kwa kujificha, usiwaone. Usiwastuke! Kwani Bwana Mungu wako yuko katikati yako, naye ni Mungu mkubwa anayeogopesha. Yeye Bwana Mungu wako atayang'oa hayo mataifa mbele yako moja kwa moja, kwani hutaweza kuwamaliza upesi, nyama wa porini wasizidi kuwa wengi kwako. Bwana Mungu wako atawatoa mbele yako na kuwahangaisha mahangaiko makubwa, hata waishe kuangamizwa. Nao wafalme wao atawatia mikononi mwako, nawe sharti uyatoweshe majina yao chini ya mbingu; hakuna atakayeweza kusimama mbele yako, mpaka uwaangamize. Vinyago vya miungu yao vya kuchongwa sharti mviteketeze kwa moto, usitamani kuzichukua fedha na dhahabu vilizotiwa, usinaswe nazo, kwani zinamchukiza Bwana Mungu wako. Wala usiingize nyumbani mwako machukizo kama hayo, usitiwe nawe mwiko wa kuwapo kama wao, ila na yakuchukize kabisa na kukutapisha kwa kuwa yenye mwiko. Maagizo yote, mimi ninayokuagiza leo, sharti myaangalie, myafanye, mpate kupona na kuwa wengi na kuiingia hiyo nchi, Bwana aliyowaapia baba zenu, mwichukue, iwe yenu. Zikumbuke njia zote, Bwana Mungu wako alizokuendesha nyikani hii miaka 40, akunyenyekeze na kukujaribu, ayajue yaliyomo moyoni mwako, kama utayaangalia maagizo yake, au kama utayakataa. Akakunyenyekeza na kukutia njaa, lakini kisha akakulisha Mana, usizozijua wewe, wala baba zako hawakuzijua, akajulisha, ya kama mtu hataishi kwa chakula tu, ila kwa kila neno linalotoka kinywani mwa Bwana. Nguo zako hazikuchakaa mwilini pako, wala miguu yako haikuvimba hii miaka 40. Hapo ujue moyoni mwako, ya kuwa Bwana Mungu wako anakuchapa, kama mtu anavyomchapa mwanawe. Kwa hiyo yaangalie maagizo ya Bwana Mungu wako, upate kuzishika njia zake na kumcha. Kwani Bwana Mungu wako ndiye atakayekuingiza katika nchi hiyo njema iliyo nchi yenye vijito na visima na viziwa vya maji yatokeayo mabondeni na vilimani. Ni nchi yenye ngano na mawele na mizabibu na mikuyu na mikomamanga, ni nchi yenye michekele iletayo mafuta, nazo asali ziko. Ni nchi, utakakokula chakula na kushiba sana, kwani hutakosa cho chote; ni nchi yenye mawe ya chuma, nazo shaba utazichimbua ndani ya milima yake. Kwa hiyo utakapokula na kushiba sharti umtukuze Bwana Mungu wako kwa ajili ya nchi hiyo njema, aliyokupa. Jiangalie, usimsahau Bwana Mungu wako, ukiacha kuyaangalia maagizo yake na maamuzi yake na maongozi yake, mimi ninayokuagiza leo. Hapo, utakapokula na kushiba, tena utakapojenga nyumba nzuri na kukaa humo, tena ng'ombe na mbuzi na kondoo wako watakapokuwa wengi, nazo fedha na dhahabu zako zitakapokuwa nyingi, nazo mali zako zote zitakapokuwa nyingi, jiangalie, moyo wako usijikuze, ukamsahau Bwana Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa! Naye ndiye aliyekuongoza katika ile nyika kubwa inayoogopesha sana kwa nyoka za moto na kwa nge walioko na kwa kiu iliyoko nyingi, kwa kuwa hakuna maji; lakini yeye alikutolea maji katika mwamba mgumu sana. Akakulisha nyikani Mana, baba zako wasizozijua, akunyenyekeze na kukujaribu, apate kukufanyizia mema, yawe ya mwisho ya kukupa. kama sivyo, ungalisema moyoni mwako: Nguvu zangu na uwezo wa mikono yangu ndizo zilizonipatia mali hizi. Mkumbuke Bwana Mungu wako, kwani yeye ndiye anayekupa nguvu za kujipatia mali, alishikize Agano lake, alilowaapia baba zako, kama inavyoelekea leo. Lakini itakapokuwa, umsahau Bwana Mungu wako na kufuata miungu mingine, uitumikie na kuitambikia, ninawashuhudia leo, ya kuwa mtaangamia kabisa. Kama Bwana alivyoyaangamiza yale mataifa mbele yenu, ndivyo, mtakavyoangamia nanyi, kwa kuwa hamkuisikiliza sauti ya Bwana Mungu wenu. Sikiliza, Isiraeli! Unataka leo kuuvuka Yordani, uingie huko kuchukua nchi ya mataifa yenye watu wengi walio na nguvu kuliko wewe, nayo miji ni mikubwa yenye maboma yanayofika hata mbinguni. Wako nao wana wa Anaki walio watu wengi na warefu, wewe nawe unawajua, ukasikia mwenyewe, watu wakisema: Yuko nani atakayesimama mbele ya wana wa Anaki? Kwa hiyo ujue leo hivi, ya kama Bwana Mungu wako ndiye atakayekutangulia kuvuka kuwa moto ulao, awaangamize na kuwaangusha chini mbele yako, upate kuwafukuza na kuwatowesha upesi, kama Bwana alivyokuambia. Bwana Mungu wako atakapowakimbiza mbele yako, usiseme moyoni mwako kwamba: Ni kwa ajili ya wongofu wetu, Bwana akituleta huku, tuichukue nchi hii, iwe yetu. Kwani ni kwa ajili ya uovu wao hao wamizimu, Bwana akiwafukuza mbele yako. Si kwa wongofu wako wala kwa unyofu wa moyo wako, wewe ukiingia kwao kuichukua nchi yao, iwe yako, ila kwa ajili ya uovu wao hao wamizimu Bwana Mungu wako amewafukuza mbele yako, alishikize lile neno, alilowaapia baba zako Aburahamu na Isaka na Yakobo. Kwa hiyo jua, ya kuwa si kwa ajili ya wongofu wako, Bwana Mungu wako akikupa nchi hiyo njema kuichukua, iwe yako. Kwani ninyi m watu wenye kosi ngumu. Kumbuka, usisahau, ulivyomkasirisha Bwana Mungu wako nyikani! Tangu siku ile, ulipotoka katika nchi ya Misri, mpaka mlipofika mahali hapa, mlikuwa mkikataa kumtii Bwana. Nako kule Horebu mlimkasirisha Bwana, Bwana akawatolea makali yake alipotaka kuwaangamiza. Ilikuwa hapo, nilipopanda mlimani kuzichukua zile mbao za mawe zilizokuwa mbao za Agano, Bwana alilolifanya nanyi. Nami nikakaa mlimani siku 40 mchana kutwa na usiku kucha, sikula chakula, wala sikunywa maji. Ndipo, Bwana aliponipa mbao mbili za mawe zilizoandikwa kwa kidole cha Mungu maneno yote sawasawa, kama Bwana alivyoyasema nanyi huko mlimani toka motoni siku ile, mlipokusanyika. Zile siku 40 za mchana kutwa na usiku kucha zilipokwisha, Bwana akanipa zile mbao mbili za mawe, ndio mbao za Agano. Kisha Bwana akaniambia: Ondoka, ushuke upesi, kwani walio ukoo wako, uliowatoa Misri, wamefanya vibaya, wameondoka upesi katika hiyo njia, niliyowaagiza, wakajitengenezea kinyago cha kuyeyushwa. Tena Bwana akaniambia kwamba: Nilipowatazama watu hawa, nikawaona kuwa watu wenye kosi ngumu. Niache, niwaangamize na kulifuta jina lao, litoweke chini ya mbingu! Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa lenye nguvu, tena lenye watu wengi kuliko wao. Ndipo, nilipogeuka na kushuka mlimani, nao mlima ulikuwa ukiwaka moto, nazo hizo mbao mbili za Agano zilikuwa katika mikono yangu miwili. Nilipotazama niliona, ya kuwa mlimkosea Bwana Mungu wenu kwa kujifanyia kinyago cha ndama kilichoyeyushwa; ndivyo, mlivyoondoka upesi katika hiyo njia, Bwana aliyowaagiza. Ndipo, nilipozikamata zile mbao mbili, nikazitupa, zitoke katika mikono yangu miwili, nikazivunja hivyo machoni penu. Nikamwangukia Bwana kama ile mara ya kwanza siku 40 mchana kutwa na usiku kucha, sikula chakula, wala sikunywa maji kwa ajili ya makosa yenu yote, mliyoyakosa na kufanya yaliyokuwa mabaya machoni pake Bwana, yaliyomkasirisha. Kwani niliyaogopa makali na machafuko ya Bwana kwa hivyo, alivyowakasirikia akitaka kuwaangamiza ninyi; lakini Bwana akanisikia hata mara hiyo. Naye Haroni Bwana akamkasirikia sana, akataka kumwangamiza naye; lakini nikambembeleza siku hiyo hata kwa ajili yake Haroni. Kisha nikaichukua ile ndama, mliyoitengeneza kwa ukosaji wenu, nikaiteketeza kwa moto nilipokwisha kuikatakata na kuiponda kabisa, mpaka ikawa vumbi tupu; kisha nikayatupa hayo mavumbi yake katika kijito kilichoshuka mlimani. Nako Tabera na Masa na kwenye Makaburi ya Uchu mkamkasirisha Bwana, alipowaagiza kutoka Kadesi-Barnea akisema: Pandeni, mwichukue hiyo nchi, nitakayowapa, mkakataa kukitii kinywa cha Bwana Mungu wenu, maana hamkumtegemea, wala hamkuisikia sauti yake. Mlikuwa wenye kukataa kumtii Bwana tangu siku hiyo, ninapowajua ninyi. Hapo, nilipokuwa nimemwangukia Bwana hizo siku 40 mchana kutwa na usiku kucha, nilizolala chini, kwa kuwa Bwana alitaka kuwaangamiza ninyi, nikambembeleza Bwana kwamba: Bwana Mungu wangu, usiwaangamize walio ukoo wako, uliojipatia kuwa wako na kuwakomboa kwa ukuu wako ulipowatoa Misri kwa mkono wako wenye nguvu. Wakumbuke watumishi wako Aburahamu na Isaka na Yakobo, usiungalie ugumu wa watu hawa, wala uovu wao, wala ukosaji wao, watu wa nchi hiyo, ulikotutoa, wasiseme: Bwana hakuweza kuwaingiza katika nchi ile, aliyowaagia, ila aliwatoa tu kwa kuwachukia, apate kuwaua nyikani. Nao ni ukoo wako, uliojipatia kuwa wako mwenyewe ulipowatoa kwa nguvu zako kuu na kwa kuukunjua mkono wako. Wakati huo Bwana akaniambia: Jichongee mbao mbili za mawe kama zile za kwanza! Kisha panda kwangu huku mlimani! Jitengenezee nalo sanduku la mti! Kisha nitaziandika hizo mbao yale maneno yaliyokuwa yameandikwa katika zile mbao za kwanza, ulizozivunja, kisha uziweke sandukuni. Ndipo, nilipotengeneza sanduku la mti wa mgunga, nikachonga mbao mbili za mawe kama zile za kwanza, kisha nikapanda mlimani nikizishika hizo mbao mbili mkononi mwangu. Akaziandika hizo mbao kuwa kama mwandiko wa kwanza yale maneno kumi, Bwana aliyowaambia ninyi huko mlimani toka motoni siku hiyo, mlipokusanyika; kisha Bwana akanipa. Ndipo, nilipogeuka, nikatelemka mlimani, nikaziweka hizo mbao katika sanduku, nililolitengeneza, zikakaa humo, kama Bwana alivyoniagiza. Kisha wana wa Isiraeli wakaondoka visimani kwa wana wa Yakani, wakaenda Mosera; ndiko, Haroni alikokufa, akazikwa huko, naye mwanawe Elazari akawa mtambikaji mahali pake. Walipoondoka huko wakaenda Gudigoda, tena toka Gudigoda, wakaenda Yotibata, ndiyo nchi yenye vijito vya maji. Siku zile Bwana akalitenga shina la Lawi, walichukue Sanduku la Agano la Bwana, tena wasimame mbele ya Bwana kumtumikia na kubariki watu kwa Jina lake, kama wanavyofanya hata leo. Kwa hiyo lawi asipate kwa ndugu zake fungu la nchi kuwa lake, kwani Bwana ndiye fungu lake mwenyewe, kama Bwana Mungu wako alivyosema. Mimi niliposimama huko mlimani kama siku zile za kwanza siku 40 mchana kutwa na usiku kucha, Bwana akanisikia hata mara hiyo, Bwana hakutaka kuwaangamiza ninyi, kwa hiyo Bwana akaniambia: Inuka, uende na kuwatangulia watu, waiingie hiyo nchi kuichukua, iwe yao, kwani ndiyo, niliyowaapia baba zao kuwapa. Sasa, Isiraeli, yako mambo gani, Bwana Mungu wako anayokutakia, isipokuwa kumcha Bwana Mungu wako na kuzishika njia zake zote na kumpenda na kumtumikia Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kuyashika maagizo ya Bwana na maongozi yake, mimi ninayokuagiza leo, upate kuona mema? Tazama, mbingu nazo mbingu za mbingu nayo nchi pamoja nayo yote yaliyomo ni yake Bwana. lakini Bwana alishikamana na baba zenu tu kwa kuwapenda, akawachagua ninyi mlio wazao wao waliokuwako nyuma yao akiwatoa katika makabila yote, kama inavyoelekea leo. Kwa hiyo itahirini mioyo yenu, tena msizishupaze kosi zenu! kwani Bwana Mungu wenu ni Mungu wa miungu, ni Bwana wa mabwana, ni Mungu mkubwa atishaye kwa matendo ya nguvu, hapendelei uso wa mtu, hachukui mapenyezo. Huamulia waliofiwa na wazazi nao wajane, hupenda wageni, awape chakula na nguo. Kwa hiyo nanyi wapendeni wageni, kwani nanyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Mwogope Bwana Mungu wako, umtumikie, ugandamane naye. Napo utakapoapa litaje Jina lake! Yeye ni shangilio lako na Mungu wako aliyekufanyizia yale matendo makuu yaliyotisha, uliyoyaona kwa macho yako. Baba zako waliposhukia Misri walikuwa watu 70, na sasa Bwana Mungu wako amekufanya kuwa wengi kama nyota za mbinguni. Kwa hiyo umpende Bwana Mungu wako na kuyaangalia mambo yake yanayopasa, uyaangalie siku zote, maongozi yake na maamuzi yake na maagizo yake! Ndipo, mtakapomtambua na leo; kwani sisemi na wana wenu, maana hawayajui, wala hawakuyaona mapatilizo ya Bwana Mungu wenu na matendo yake makuu na nguvu za kiganja chake na uwezo wa mkono wake, alipoukunjua. na vielekezo vyake na matendo yake yote, aliyomfanyizia Farao, mfalme wa Misri, nao wenyeji wa nchi yake kule kwao Misri, nayo aliyovifanyia vikosi vya Farao na farasi wake na magari yake, aliowafurikishia maji ya Bahari Nyekundu ya kuwatosa, walipokimbia, wawafikilie ninyi, Bwana akawaangamiza, wasionekane tena hata leo. Hawakuyaona nayo, aliyowafanyia ninyi nyikani, mpaka mfike mahali hapa, nayo aliyowafanyia Datani na Abiramu, wana wa Eliabu, mwana wa Rubeni, nchi ilipowaasamia na kuwameza wao na nyumba zao na mahema yao pamoja nao wote waliosimama upande wao kwa miguu yao katikati yao Waisiraeli wote. Ila ninasema nanyi, kwani macho yenu ndiyo yaliyoyaona hayo matendo makuu yote, Bwana aliyoyafanya. Kwa hiyo yaangalieni maagizo yote, mimi ninayowaagiza leo, mpate nguvu za kuiingia hiyo nchi na kuichukua, iwe yenu, maana mnaivukia kuichukua, iwe yenu, nanyi siku zenu zipate kuwa nyingi katika nchi hiyo, Bwana aliyowaapia baba zenu kuwapa wao nao wa uzao wao, hiyo nchi ichuruzikayo maziwa na asali. Kwani hiyo nchi, utakayoiingia kuichukua, iwe yako, haifanani na nchi ya Misri, mlikokaa: ulipopanda mbegu huko hukuwa na budi kuzinywesha kwa kazi za miguu yako, zipate kuwa shamba la mboga. Lakini hiyo nchi, mtakayovukia kuichukua, iwe yenu, ni nchi yenye milima na mabonde, nayo hunyweshwa maji ya mvua za mbinguni. Nayo ni nchi, Bwana Mungu wako anayoipatia yaipasayo, nayo macho yake Bwana Mungu wako hayakomi kuitazama tangu mwanzo wa mwaka hata mwisho wa mwaka. Itakuwa, mtakapoyasikia vema maagizo yangu, mimi ninayowaagiza leo, mmpende Bwana Mungu wenu na kumtumikia kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote: nitatoa mvua za nchi yenu, siku zake zitakapotimia, mvua ya vuli na ya masika, upate kuzivuna ngano zako na mvinyo zako na mafuta yako. Nao nyama wako wa kufuga nitawapa majani maporini, upate kula na kushiba. Jiangalieni tu, mioyo yenu isidanganyike, mmwache Bwana, mkaenda kutumikia miungu mingine na kuitambikia. Mtakapofanya hivyo, makali ya Bwana yatawawakia ninyi, azifunge mbingu, mvua isinye, nchi isitoe mazao yake; ndipo, mtakapoangamia upesi, mtoweke katika hiyo nchi njema, Bwana atakayowapa. Kwa hiyo haya maneno yangu yawekeni mioyoni na rohoni mwenu! Tena yafungeni mikononi penu kuwa kielekezo, yawe napo mapajini penu katikati ya macho yenu! Yafundisheni watoto wenu na kuyasema nao ukikaa nyumbani mwako, ukienda safari zako, ukitaka kulala, hata ukiamka! Yaandike vizingitini namo milangoni nyumbani mwako! Ndipo, siku zenu nazo siku za wana wenu zitakapokuwa nyingi katika hiyo nchi, Bwana Mungu wenu aliyowaapia baba zenu kuwapa, iwe yao siku zote, mbingu zitakazokuwa juu ya nchi. Kwani mtakapoyaangalia vema haya maagizo yote, mimi ninayowaagiza ninyi, myafanye na kumpeda Bwana Mungu wenu na kuzishika njia zake na kugandamana naye, ndipo, Bwana atakapoyafukuza hayo mataifa yote mbele yenu, mchukue nchi za mataifa walio wengi na wenye nguvu kuliko ninyi. Ndipo, mahali po pote, nyayo za miguu yenu zitakapopakanyaga, patakapokuwa penu, mpaka wenu utoke nyikani na Libanoni nako kwenye lile jito kubwa la Furati, ufike kwenye bahari ya machweoni kwa jua. Hatakuwako mtu atakayeweza kusimama mbele yenu, kwani Bwana Mungu wenu atawastusha, wawaogope ninyi katika nchi zote, mtakazozikanyaga, kama alivyowaambia ninyi. Tazameni, leo hivi mimi ninaweka mbele yenu mbaraka na kiapizo: mbaraka mtaipata mtakapoyasikia maagizo ya Bwana Mungu wenu, mimi ninayowaagiza leo. Lakini kiapizo kitawapata, msipoyasikia maagizo ya Bwana Mungu wenu, mwondoke katika njia hiyo, mimi ninayowaagiza leo, mkafuata miungu mingine, msiyoijua. Hapo, Bwana Mungu wako atakapokuingiza katika nchi hiyo, wewe utakayoiingia kuichukua, iwe yako, ndipo utoe mbaraka juu ya mlima wa Gerizimu, nacho kiapizo juu ya mlima wa Ebali Milima hii iko ng'ambo ya huko ya Yordani nyuma ya njia inayokwenda machweoni kwa jua katika nchi ya Wakanaani wanaokaa katika nyika inayoelekea Gilgali, ni huko kando ya kimwitu cha More. Kwani ninyi mtauvukia Yordani kuichukua hiyo nchi, iwe yenu, Bwana Mungu wenu atakayowapa, nanyi mtaichukua, iwe yenu kweli, kisha mtaikaa. Kwa hiyo angalieni, myafanye haya maongozi na maamuzi yote, mimi ninayoyaweka leo mbele yenu. Haya ndiyo maongozi na maamuzi, mtakayoyaangalia, myafanye katika hiyo nchi, Bwana Mungu wa baba zako atakayokupa, uichukue, iwe yako siku zote, mtakazoishi huku nchini. Sharti mpaangamize kabisa mahali pote, wamizimu mtakaowafukuza walipoitumikia miungu yao juu ya milima mirefu nako vilima, tena chini ya miti yenye majani mengi. Sharti mpabomoe pao pa kutambikia, nazo nguzo zao za mawe za kutambikia mzivunje, nayo miti yao ya Ashera mwiteketeze, navyo vinyago vya miungu yao vya kuchongwa mvikatekate, myatoweshe majina yao mahali pale palipokuwa pao. Bwana Mungu wenu msimfanyizie hivyo, ila mahali pale pamoja, Bwana Mungu wenu atakapopachagua katika mashina yote pa kuliwekea Jina lake, likae papo hapo, ndipo papasapo, mpaingie mtakapomtafuta. Tena ndipo papasapo, mpapeleke ng'ombe zenu za tambiko za kuteketezwa nzima na ng'ombe zenu nyingine za tambiko na mafungu yenu ya kumi na vipaji vya mikono yenu vya tambiko vya kunyanyuliwa na matoleo ya kuyalipa mliyoyaapa na matoleo yenu, mtakayoyatoa kwa kupenda wenyewe, na wana wenu wa kwanza wa ng'ombe na wa mbuzi na wa kondoo. Napo ndipo papasapo, mle mbele ya Bwana Mungu wenu mtakapomtambikia kwa kuyafurahia yote, iliyoyachukua mikono yenu ninyi nayo yao waliomo nyumbani mwenu, kwa kuwa Bwana Mungu wako alikubariki. Msiyafanye haya yote, tunayoyafanya sisi leo huku, kila mtu akiyafanya yanyokayo machoni pake yeye. Kwani hamjaingia bado kwenye kituo wala katika nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe yako. Lakini mtauvuka Yordani, mpate kukaa katika nchi hiyo, Bwana Mungu wenu atakayowapa, iwe fungu lenu; ndiko, atakakowapatia kupumzika kwa kuwashinda adui zenu wote pande zote, mkae na kutulia. Kisha mahali pale, Bwana Mungu wenu atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake, sharti mpeleke hapo yote, mimi ninayowaagiza leo: ng'ombe zenu za tambiko za uteketezwa nzima na ng'ombe zenu nyingine za tambiko na mafungu yenu ya kumi na vipaji vya mikono yenu vya tambiko vya kunyanyuliwa, nayo yote ya kuyalipa, mliyoyaapa kumtolea Bwana kwa kupenda wenyewe. Tena ndipo, mtakapomfurahia Bwana Mungu wenu, ninyi na wana wenu wa kiume na wa kike na watumishi wenu wa kiume na wa kike, nao Walawi watakaokaa milangoni kwenu, kwani wao hawatapata fungu la nchi litakalokuwa lao. Jiangalie, usitoe ng'ombe zako za tambiko za kuteketezwa nzima mahali po pote, utakapopaona! Ila mahali pale pamoja tu, Bwana atakapopachagua katika moja lao mashina yako, ndipo papasapo, utolee hapo ng'ombe zako za tambiko za kuteketezwa nzima, tena ndipo papasapo, uyafanye yote, mimi ninayokuagiza. Lakini roho yako ikiwa na uchu wa nyama tu, utazichinja na kuzila malangoni pako po pote kwa mbaraka ya Bwana Mungu wako aliyekupa hizo nyama; mwenye uchafu na mwenye kutakata atazila, kama ni za paa au kama ni za kulungu. Damu tu msiile, ila mwimwage mchangani kama maji. Lakini ni mwiko kula malangoni pako fungu la kumi la ngano zako, nalo la mvinyo zako mbichi, nalo la mafuta yako, nao wana wa kwanza wa ng'ombe wako nao wana wa kwanza wa mbuzi wako na wa kondoo wako, nayo yo yote ya kuyalipa uliyoyaapa, nayo matoleo yako, utakayoyatoa kwa kupenda mwenyewe, navyo vipaji vya mikono yako vya tambiko vya kunyanyuliwa. Haya yote utayala mbele ya Bwana Mungu wako mahali pale tu, Bwana Mungu wako atakapopachagua; hapo na uyale wewe na wana wako wa kiume na wa kike na watumishi wako wa kiume na wa kike, naye Mlawi aliopo malangoni pako, upate kuyafurahia mbele ya Bwana yote, mikono yako iliyoyachukua. Jiangalie tu, usimwache Mlawi siku zote, utakazokuwapo katika nchi yako! Bwana Mungu wako atakapoipanua mipaka yako, kama alivyokuambia, nawe utakaposema: Nataka kula nyama, kwani roho yangu ina uchu wa nyama, basi, na ule nyama kwa huo uchu wote wa roho yako. Kama mahali pale, Bwana Mungu atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake, patakuwa mbali kutoka kwako, basi, na utoe wa kuchinja katika ng'ombe wako au katika mbuzi na kondoo wako, Bwana aliokupa, ule nyama, kama nilivyokuagiza, malangoni pako, uukomeshe uchu wote wa roho yako. Kama nyama za paa na za kulungu zinavyoliwa, hivyo ndivyo, utakavyozila hizo nyama nazo, mwenye uchafu na mwenye kutakata watazila pamoja. Lakini ushike mwiko huu tu, usile damu! Kwani damu ndiyo yenye roho, haifai ukiila roho pamoja na nyama. Kwa hiyo usiile, ila uimwage mchangani kama maji. Usiile, upate kuona mema wewe na wanao watakaokuwapo nyuma yako, ukiyafanya yanyokayo machoni pake Bwana. Ni vipaji vyako vitakatifu tu na malipo yao, uliyoyaapa, ndiyo uyachukue kwenda mahali pake, Bwana atakapopachagua. Hapo pa kumtambikia Bwana Mungu wako ndipo papasapo, uzitoe ng'ombe zako za tambiko za kuteketezwa nzima, nyama pamoja na damu. Nazo damu za ng'ombe zako nyingine za tambiko sharti zimwagwe hapo pa kumtambikia Bwana Mungu wako, lakini nyama utazila. Angalia, uyasikie vema haya maneno, mimi ninayokuagiza, upate kuona mema kale na kale, wewe na wanao watakaokuwako nyuma yako, utakapoyafanya yaliyo mema nayo yanyokayo machoni pa Bwana Mungu wako. Bwana Mungu wako atakapowang'oa mbele yako wamizimu hao, ambao utaingia kwao kuichukua nchi yao, iwe yako, ukiwafukuza, upate kukaa katika nchi yao, jiangalie, usinaswe, kwamba uwafuate wao, wakiisha kuangamizwa mbele yako, wala usiulizeulize habari za miungu yao kwamba: Hao wamizimu walivyoitumikia miungu yao, ndivyo, nitakavyofanya nami. Usimfanyizie Bwana Mungu wako hivyo! Kwani yote yaliyo matapisho kwake Bwana kwa kuyachukia waliifanyizia miungu yao, kwani nao wana wao wa kiume na wa kike waliitolea miungu yao na kuwateketeza motoni. Maneno haya yote, mimi ninayowaagiza ninyi, sharti myaangalie, myafanye. Msiyaongeze, wala msiyapunguze! Atakapoinuka katikati yako mfumbuaji au mwota ndoto na kukutolea kielekezo au kioja, nacho hicho kielekezo au kioja, alichokuambia, kitakapotimia, ndipo, atakapokuambia: Twende, tufuate miungu mingine, msiyoijua, tuitumikie! Lakini usiyasikie maneno ya mfumbuaji huyo au ya mwota ndoto huyo! Kwani Bwana Mungu wenu atawajaribu tu, ajue, kama ninyi mnampenda Bwana Mungu wenu kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote. Mfuateni Bwana Mungu wenu na kumcha, myashike maagizo yake na kuisikia sauti yake, mmtumikie na kugandamana naye! Lakini yule mfumbuaji au yule mwota ndoto sharti auawe, kwa kuwa amesema, mmwache Bwana Mungu wenu aliyewatoa ninyi katika nchi ya Misri na kuwakomboa nyumbani, mlimokuwa watumwa; naye yule alitaka kukudanganya, uondoke katika hiyo njia, Bwana Mungu wako aliyokuagiza kuishika. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako! Itakuwa, ndugu yako aliyezaliwa na mama yako au mwanao wa kiume au wa kike au mkeo anayekaa kfuani pako au mwenzako, unayempenda, kama unavyojipenda mwenyewe, akuhimize penye njama kwamba: Twende, tutumikie miungu mingine, usiyoijua wewe, wasiyoijua nao baba zako! Nayo ndiyo iliyomo miongoni mwa miungu ya makabila yanayoaa na kuwazunguka ninyi pande zote, wengine wao wanakukalia karibu, wengine mbali toka mwanzo wa nchi hata mwisho wake. Basi itakapokuwa hivyo, usimwitikie, wala usimsikie, jicho lako lisimwonee machungu, usimhurumie, wala usimfiche, ila mwue kabisa! Mkono wako sharti uwe wa kwanza wa kumua, kisha mikono yao watu wote na ifuate. Sharti umpige mawe, hata afe! Kwani alijaribu kukudanganya, umwache Bwana Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri nyumbani ulimokuwa mtumwa. Nao Waisiraeli wote watakapovisikia wataogopa, wasiendelee kufanya kwako mabaya kama nayo. Itakuwa, upate habari ya mmojawapo katika miji yako, Bwana Mungu wako atakayokupa ya kukaa humo, kwamba: Wako watu wasiofaa waliotoka katikati yako, waliowadanganya wenyeji wa miji yao kwamba: Twende, tutumikie miungu mingine, msiyoijua! Basi, utakapovisikia, sharti utafute na kuchunguza na kuuliza vema; kisha utakapoona, ya kama neno hili ni la kweli, ikaelekea, ya kama tapisho hilo limefanyika kweli katikati yako, huna budi kuwapiga wenyeji wa mji huo kwa ukali wa upanga na kuutia huo mji pamoja nayo yote yaliyomo mwiko wa kuwapo, nao nyama wao wa kufuga sharti uwaue kwa ukali wa upanga. Kisha na uyakusanye mateka yote katikati ya uwanja wake, uuteketeze huo mji kwa moto pamoja na amteka yake yote kuwa ng'ombe ya tambiko ya Bwana Mungu wako ya kuteketezwa yote nzima, uwe chungu ya majivu kale na kale, usijengwe tena. Katika vile vyote vilivyotiwa mwiko wa kuwapo kisioneke cho chote kitakachogandamana na mkono wako, Bwana ayatulize tena makali yake yaliyowaka moto, akuonee machungu, akuhurumie na kukufanya kuwa wengi, kama alivyowaapia baba zako. haya yatakuwa, utakapoisikia sauti ya Bwana Mungu wako na kuyaangalia maagizo yake yote, mimi ninayokuagiza leo, uyafanye yanyokayo machoni pake Bwana Mungu wako. Ninyi m watoto wake Bwana Mungu wenu; kwa hiyo msijichanje chale, wala msizinyoe nyushi katikati ya macho yenu kwa ajili ya mfu! Kwani ninyi m watu watakatifu wa Bwana Mungu wako, maana Bwana akikuchagua kuwa kabila lililo lake mwenyewe kuliko makabila yote yakaayo huku nchini. Usile cho chote kinachotapisha! Hawa ndio nyama, mtakaowala: ng'ombe, kondoo na mbuzi, kulungu na paa na funo na mbarapi na kuro na pofu na swala. Nyama wote wenye kwato zilizopasuka na kutengeka kabisa kuwa kwato mbili, kama ni wenye kucheua, ndio, mtakaowala miongoni mwa nyama. Lakini nao hao msiwale miongoni mwao wanaocheua namo miongoni mwao walio wenye kwato zilizopasuka na kutengeka: ngamia na sungura na pelele. Kweli wanacheua, lakini hawapasui kwato, kwa hiyo ni mwiko kwenu. Naye nguruwe, kweli anayapasua makwato, lakini hacheui; kwa hiyo ni mwiko kwenu. Nyama zao hao msizile, nayo mizoga yao msiiguse. Katika nyama wote waliomo majini mtakula hawa: wote wenye mapezi na magamba mtawala; lakini wote wasio wenye mapezi na magamba msiwale! ni mwiko kwenu. Kila ndege mwenye kutakata mtakula. Lakini wao, mtakaoacha kula nyama zao, ni hawa: kozi na pungu na furukombe, na tumbuzi na mwewe na ngusu na ndugu zake, na makunguru yote na ndugu zao, na mbuni na kinega na dudumizi na kipanga na ndugu zake, na mumbi na bundi na yangeyange, na korwa na tai na shakwe, na korongo na kitwitwi na ndugu zake na hudihuda na popo. Wadudu wote wenye mabawa wanaotambaa ni mwiko kwenu, hawaliwi. Ndege wote wenye kutakata mtakula. Msile kibudu cho chote! Mgeni aliomo malangoni mwako utampa, ale, au utakiuza kwa mtu wa kimizimu. Kwani ninyi m watu watakatifu wa Bwana Mungu wenu. Kitoto cha mbuzi usikipike katika maziwa ya mama yake. Mwaka kwa mwaka sharti utoe fungu la kumi la mapato yote ya mbegu zako zitakazotoka shambani. Hili fungu la kumi ulile mbele ya Bwana Mungu wako mahali pale, atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake, nalo hilo fungu la kumi ulitolee ngano zako na mvinyo zako mbichi na mafuta yako, tena wana wa kwanza wa ng'ombe nao wa mbuzi na kondoo wako, upate kujifunza kumcha Bwana Mungu wako siku zote. Kama safari ya kutoka kwako kwenda huko itakuwa ndefu zaidi, usiweze kuyapeleka hayo matoleo, kwa kuwa ni mbali zaidi kutoka kwako kwenda mahali pale, Bwana Mungu wako atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake, basi, hapo Bwana Mungu wako atakapokubariki, yale matoleo yageuze kuwa fedha, kisha hizo fedha zifunge mkononi mwako, upate kwenda nazo mahali pale, Bwana Mungu wako atakapopachagua. Ndipo, utakapoweza kujipatia kwa hizo fedha yote, roho yako itakayotunukia, ng'ombe na mbuzi na kondoo na mvinyo na vileo nayo mengine yote, roho yako itakayoyapenda, ujipatie, kisha utakula hapo mbele ya Bwana Mungu wako, mfurahiwe pamoja wewe nao waliomo nyumbani mwako. Naye Mlawi atakayekuwapo malangoni pako usimwache, kwani hana fungu la nchi kwako lililo lake mwenyewe. Miaka mitatu itakapopita, mafungu yote ya kumi utakayoyatolea mapato yako ya mwaka huo, uyaweke malangoni pako. Kisha Walawi, kwa kuwa kwako hawana fungu lao la nchi lililo lao wenyewe, na waje pamoja na wageni, nao wliofiwa na wazazi, nao wajane waliomo malangoni mwako, na waje, wale, washibe! Hivyo ndivyo, Bwana Mungu wako atakavyokubarikia kazi zote za mikono yako, utakazozifanya. Miaka saba itakapopita, mwachiliane madeni! Nalo jambo hili la kuachaliana madeni liwe hivyo: kila mkopeshaji aliyemkopesha mwenziwe asimwendee kumdai huyo mwenziwe au ndugu yake, kwani maachilio ya Bwana yametangazwa. Asiye wa Kiisiraeli utaweza kumwendea, umtoze, lakini aliye ndugu yako utamwachilia. Kweli kwako asingekuwako mkopaji, kwani Bwana atakubariki sana katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe fungu lako mwenyewe, kama wewe ungeisikia tu sauti ya Bwana Mungu wako, uyaangalie na kuyafanya hayo maagizo yote, mimi ninayokuagiza leo. Kwani Bwana Mungu wako atakubariki, kama alivyokuambia. Kwa hiyo utaweza kukopesha mataifa mengi, lakini mwenyewe hutakopa; hivyo utatawala mataifa mengi, lakini wewe hawatakutawala. Itakapokuwa, ndugu yako mmoja aliopo malangoni pako pawapo pote katika nchi yako, Bwana Mungu wako atakayokupa, akose mali, usiushupaze moyo wako, wala usiufunge mkono wako ukimnyima ndugu yako anayetaka kukukopa. Ila umfungulie mkono wako na kumkopesha yatoshayo kuukomesha ukosefu wake, alioukosa. Jiangalie sana, moyoni mwako lisiingie shauri lisilofaa kabisa la kwamba: Mwaka wa saba, ndio mwaka wa kuachilia madeni, uko karibu, ukamtazama ndugu yako anayetaka kukukopa kwa macho yenye ubaya wa kumnyima; hili kosa litakukalia hapo, atakapomlilia Bwana kwa ajili yako. Kwa hiyo sharti ujihimize kumpa, wala moyo wako usiwe mbaya kwa kumpa; kwani kwa jambo kama hili Bwana Mungu wako atakubarikia matendo yako yote na mapato yote ya mikono yako. Kwani wenye kukosa mali hawatakoma katika nchi hii; kwa sababu hii mini ninakuagiza kwamba: Ndugu yako aliye mnyonge na mkosa mali kwako katika nchi yako umfungulie mkono wako kabisa! Ndugu yako mume au mke wa Kiebureo akijiuza kwako, akakutumikia miaka sita, sharti umwache katika mwaka wa saba, atoke kwako kuwa mwungwana tena. Tena ukimwacha, atoke kwako kuwa mwungwana tena, usimwache, ajiendee mikono mitupu! Ila umgawie mali kwenda nazo, ukitoa mbuzi na kondoo na mapato ya purio lako, nayo ya kamulio lako. Kwa hivyo, Bwana Mungu wako alivyokubariki, umgawie naye. Ukumbuke, ya kama ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, naye Bwana Mungu wako akakukomboa. Kwa sababu hii mimi ninakuagiza leo neno hili. Lakini atakapokuambia: Sitaki kutoka kwako, kwani ninakupenda wewe nao waliomo nyumbani mwako, kwa kuwa ninaona mema kwako, basi, uchukue shazia, ulitoboe sikio lake nalo, kisha umpigilie hivyo mlangoni; ndipo, atakapokuwa mtumwa wako kale na kale. Hata kijakazi utamfanyizia vivyo hivyo. Usiyawazie kuwa magumu kumwacha, aondoke kwako kuwa mwungwana tena, kwani atakuwa amekutumikia miaka sita na kufanya kazi za watu wawili wa mshahara, naye Bwana Mungu wako atakubarikia yote, utakayoyafanya. Wana wote wa kwanza watakaozaliwa, wao wa ng'ombe wako na wa mbuzi na wa kondoo wako, kama ni wa kiume, sharti uwatakase kuwa wake Bwana Mungu wako, usimtumie kazini mwana wa kwanza wa ng'ombe wako, wala usimkate manyoya mwana wa kwanza wa kondoo wako. Ila utamla mbele ya Bwana Mungu wako, wewe pamoja nao waliomo nyumbani mwako, mwaka kwa mwaka mahali pale, Bwana atakapopachagua. Lakini akiwa mwenye kilema, kama ni kiwete au kipofu au mwenye kilema kibaya cho chote, usimchinjie Bwana Mungu wako, ila utamla malangoni pako, mwenye uchafu na mwenye kutakata pamoja, kama unavyokula paa au kulungu. Damu yake tu usiile, ila uimwage mchangani kama maji. Uangalie mwezi wa Abibu, ule sikukuu ya Pasaka ya Bwana Mungu wako! Kwani ulikuwa mwezi wa Abibu, Bwana Mungu wako alipokutoa huko Misri na usiku. Ndipo umchinjie Bwana Mungu wako kondoo ya Pasaka, ndio ng'ombe na mbuzi na kondoo, mahali pale, Bwana Mungu wako atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake. Sikukuu hiyo usile cho chote kilichochachwa, ila siku zake saba sharti ule mikate isiyochachwa kuwa mikate ya matesoni, kwa kuwa ulitoka upesiupesi na kiwogawoga katika nchi ya Misri, upate kuikumbuka siku hiyo ya kutoka katika nchi ya Misri siku zote za maisha yako. Siku hizo saba isionekane chachu katika mikate yako, wala nyama za yule kondoo, utakayemchinja siku ya kwanza jioni, zisilale usiku huo hata asubuhi. Huwezi kuichinja kondoo ya Pasaka malangoni pako miongoni mwa miji, Bwana Mungu wako atakayokupa. Ila mahali pale tu, Bwana Mungu wako atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake, ndipo, utakapoichinja kondoo ya Pasaka jioni, jua likiisha kuchwa, ndio saa zilezile zilizokuwa, ulipotoka Misri. Napo mahali pale, Bwana Mungu wako atakapopachagua, ndipo, utakapoipika na kuila palepale; kisha asubuhi yake na ugeuke nyuma kwenda hemani kwako. Siku sita sharti ule mikate isiyochachwa, nayo siku ya saba na mkutanie kumheshimu Bwana Mungu wenu; hapo msifanye kazi yo yote. Jihesabie majuma saba! Watu wakianza kukata ngano kwa miundu, ndipo uanzie kuyahesabu hayo majuma saba. Kisha na ule sikukuu ya Majuma ya Bwana Mungu wako, mkono wako ukimtolea vipaji kwa furaha ya moyo ya kuvifurahia hivyo, Bwwana Mungu wako alivyokubariki. Ndipo, mtakapofurahi mbele ya Bwana mahali pale, Bwana Mungu wako atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake, wewe na mwanao wa kiume na wa kike na mtumishi wako wa kiume na wa kike, naye Mlawi aliopo malangoni pako, nao wageni, nao waliofiwa na wazazi, nao wajane walioko kwako. Nawe ukumbuke, ya kama ulikuwa mtumwa kule Misri! Kwa hiyo angalia, uyafanye haya maongozi! Sikukuu ya Vibanda utaila siku saba utakapokwisha kuyakusanya yatokayo purioni pako na kamulioni pako. Hiyo sikukuu yako mtaifurahia, wewe na mwanao wa kiume na wa kike na mtumishi wako wa kike na wa kiume, naye Mlawi, nao wageni, nao waliofiwa na wazazi nao wajane waliopo malangoni pako. Siku saba utaila hiyo sikukuu ya Bwana Mungu wako mahali pale, Bwana atakapopachagua. Kwani Bwana Mungu wako atakubarikia mapato yako yote, nazo kazi zote za mikono yako, kwa hiyo utaweza kuwa mwenye furaha. Kila mwaka mara tatu watu wako wote walio wa kiume sharti watokee mbele ya Bwana Mungu wako mahali pale, atakapopachagua: penye sikukuu ya Mikate isiyochachwa na penye sikukuu ya Majuma na penye sikukuu ya Vibanda, lakini wasitokee mbele ya Bwana mikono mitupu! Kila mtu ashike mkononi mwake vipaji vya kuishuuru mbaraka, Bwana Mungu wako aliyokupatia. Jiwekee waamuzi na wenye amri malangoni pako pote, Bwana Mungu wako atakapokupa wewe kuwa pao mashina yako, wawaamue watu maamuzi yaongokayo. Usipotoe mashauri, wala usipendelee uso wa mtu, wala usitwae mapenyezo, kwani mapenyezo huyapofusha nayo macho yao werevu wa kweli, tena huyapotoa maneno ya waongofu. Jihimize kuyafuata yaongokayo kweli, upate kukaa uzimani na kuichukua hiyo nchi, iwe yako, Bwana Mungu wako atakayokupa. Usijipandie miti yo yote ya Ashera kandokando ya mahali pa kumtambikia Bwana Mungu wako, utakapojitengenezea. Wala usijisimamishie nguzo za mawe za kutambikia, kwani Bwana Mungu wako anazichukia. Bwana Mungu wako usimchinjie ng'ombe wala kondoo mwenye kilema au kibaya cho chote! Kwani hayo humchukiza Bwana Mungu wako. Itakuwa, malangoni mwako miongoni mwa miji, Bwana Mungu wako atakayokupa, aonekane mtu mume au mke anayefanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana Mungu wako kwa kupitana na Agano lake akienda kutumikia miungu mingine na kuitambikia, kama ni jua au mwezi au vikosi vyote vya mbinguni, nisivyokuagiza. Nawe utakapopashwa habari hizi au utakapovisikia tu, sharti utafute vema; kisha utakapoona, ya kuwa neno hilo ni kweli, ikaelekea, ya kama hilo tapisho limefanyika kweli kwao Waisiraeli, huna budi kumtoa malangoni pako huyo mtu mume au mke aliyelifanya hilo neno baya, kisha sharti mmpige mawe huyo mtu mume au mke, hata afe. Kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu mtu apaswaye na kufa ataweza kuuawa, lakini kwa ushahidi wa mtu mmoja mtu asiuawe! Mikono yao mashahidi sharti iwe ya kwanza ya kumwua, kisha mikono yao watu wote na ifuate; hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako. Itakapokuwa, shauri liwe gumu zaidi la kukushinda, kama wanastakiana manza za damu au unyang'anyi au mapigano au magomvi ya malangoni pako, basi, utainuka, upande kwenda mahali pale, Bwana Mungu wako atakapopachagua. Utakapofika kwa watambikaji Walawi na kwa mwamuzi atakayekuwako siku hizo uwaulize, nao watakukatia shauri hilo. Nawe sharti uyafanye, watakayokuambia na kukuonyesha njia mahali pale, Bwana atakapopachagua, nawe uangalie, uyafanye yote kuwa sawasawa, kama walivyokufunza. Sharti uyafuate hayo maonyo, watakayokufunza, nayo maamuzi, watakayokuambia, uyafanye hayo maneno, watakayokuonyesha, usiyaache kabisa kwenda kuumeni wala kushotoni. Itakapokuwa, mtu ajikuze, akatae kumsikia mtambikaji anayesimama huko na kumtumikia Bwana Mungu wako au mwamuzi, huyo mtu hana budi kufa; ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo kwao Waisiraeli. Ndipo, watu wote watakaovisikia watakapoogopa, wasijikuze tena. Utakapoingia katika nchi hiyo, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe yako, ukae huko, ndipo, utakaposema: Na nijiwekee mfalme, kama mataifa yote yanayokaa na kunizunguka pande zote yalivyo na wafalme. Napo hapo na umweke yule kuwa mfalme wako, Bwana Mungu wako atakayemchagua katikati ya ndugu zako; yeye ndiye, utakayemweka kuwa mfalme; mtu mgeni asiye ndugu yako hutaweza kumweka kuwa mkuu wako. Lakini angalia, asijitunzie farasi wengi, asiwarudishe watu hawa huko Misri kwa kuwa na farasi wengi, kwani Bwana aliwaambia: Msirudi tena huko na kuishika njia hii! Wala asijipatie wanawake wengi, moyo wake usirudi nyuma! Wala asijiwekee fedha nyingi sana! Lakini hapo, atakapokaa katika kiti chake cha kifalme, sharti ajiandikie mwandiko wa pili wa haya Maonyo katika kitabu na kukifuata kile cha watambikaji Walawi. Hicho kitabu sharti awe nacho, akisome siku zote za maisha yake, kusudi ajifundishe kumcha Bwana Mungu wake na kuyaangalia maneno yote ya haya Maonyo nayo ya haya maongozi, ayafanye. Asijikweze moyoni mwake kuwa mkuu kuliko ndugu zake, wala asiliache hili agizo kwenda wala kuumeni wala kushotoni, siku zake za kuwa mfalme yeye na wanawe katikati ya Waisiraeli zipate kuwa nyingi. Watambikaji Walawi, ndio shina lote la Lawi, wasipate fungu la nchi kuwa lao wenyewe kwao Waisiraeli. Ng'ombe za tambiko za Bwana za kuteketezwa nayo yampasayo Bwana kupewa yawe yao; ndiyo, watakayokula. Kweli wasiwe na fungu lililo lao kwao ndugu zao, ila Bwana mwenyewe atakuwa fungu lao, kama alivyowaambia. Lakini hii itakuwa haki yao watambikaji kwao watu watakaochinja ng'ombe ya tambiko, kama ni ng'ombe, au kama ni kondoo: sharti wampe mtambikaji mkono na mashavu mawili na matumbo. Tena malimbuko ya ngano zako nayo ya mvinyo mbichi nayo ya mafuta, nayo malimbuko ya nywele za kondoo, mkiwanyoa, na mmpe. Kwani Bwana Mungu wako amemchagua katika mashina yako yote, asimame na kutumikia katika Jina lake Bwana, yeye na wanawe siku zote. Itakapokuwa, Mlawi atoke malangoni pako pawapo pote kwao Waisiraeli, anapokaa ugenini, aende kwa tunu yote ya roho yake mahali pale, Bwana atakapopachagua, basi, na atumikie katika Jina la Bwana Mungu wake, kama ndugu zake Walawi wote wanaosimama hapo mbele ya Bwana. Watakula sawasawa na kugawiana fungu kwa fungu kuliko yale, atakayoyapata kwa kuuza mali ya baba zake. Utakapoingia katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, usijifundishe kuyafanya matapisho ya hao wamizimu. Kwako asionekane mtu atakayemtumia mwanawe wa kiume au wa kike kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa, wala asionekane mwenye kuagulia ndege na mawingu, wala mpiga bao, wala mlozi, wala mfinga nyoka kwa uganga, wala mwenye kuuliza mizimu, wala mwenye kujua uchawi wote, wala mfanya mashauri na wafu. Kwani kila ayafanyaye hayo humchukiza Bwana, naye Bwana Mungu wako anawafukuza wao mbele yako kwa ajili ya hayo machukizo. Lakini wewe sharti ukae kwa Bwana Mungu wako pasipo kumkosea. Kwani mataifa hayo, utakayoyafukuza, huwasikia waaguliao mawingu na ndege, lakini wewe Bwana Mungu wako hakukupa ruhusa kuwatumia hao. *Miongoni mwa ndugu zako wewe Bwana Mungu wako atakuinulia mfumbuaji atakayelingana na mimi, nanyi sharti mmsikie. Ni kwa ajili yao yote, uliyomwomba Bwana Mungu wako kule Horebu siku hiyo ya mkutano kwamba: Nisiendelee kuisikia sauti ya Bwana Mungu wangu na kuuona huu moto mkubwa, nisife. Ndipo, Bwana aliponiambia: Wamefanya vema waliposema hivyo. Nitawainulia mfumbuaji miongoni mwa ndugu zao atakayelingana na wewe; nitampa maneno yangu kinywani mwake, awaambie yote, nitakayomwagiza. Itakuwa, mtu akikataa kuyasikia maneno yangu, atakayoyasema katika Jina langu, mimi nitamlipisha.* Lakini mfumbuaji atakayejikuza mwenyewe na kusema neno katika Jina langu, nisilomwagiza kulisema, analolisema katika jina la mungu mwingine, huyo mfumbuaji hana budi kufa. Nawe ukiuliza moyoni mwako: Tutajuaje neno kuwa neno, Bwana asilolisema? ni hivi: mfumbuaji akisema neno kwa Jina la Bwana, lakini hilo neno haliji, wala halitimii, basi, hilo ndilo neno, Bwana asilolisema, yule mfumbuaji amelisema kwa kujikuza tu, kwa hiyo usimwogope! Bwana Mungu wako atakapokwisha kuyang'oa hayo mataifa walio wenye hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe yako, ukae mijini mwao namo nyumbani mwao, ndipo ujitengee miji mitatu katikati ya hiyo nchi yako, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe yako. Utakapojitengenezea njia za kwenda huko uanze kuigawanya mipaka ya hiyo nchi yako, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe yako mwenyewe, uitoe mafungu matatu, mwuaji apate pa kukimbilia. Nalo shauri lake mwuaji atakayekimbilia kwako, apate kupona, liwe hivyo: Itakuwa, mtu ampige mwenzake pasipo kuvijua, pasipo kuwa mchukivu wake tangu zamani. Itakuwa, kama mtu akienda na mwenzake mwituni kukata kuni, napo hapo, mkono wake ulipolipandisha shoka kukata mti, chuma kikachomoka katika kipini, kikampata mwenzake, naye akafa, basi, hapo na akimbilie miji hiyo mmojawapo, apate kupona. Naye mwenye kuilipiza hiyo damu asimkimbize huyo mwuaji kwa ajili ya moto huo unaowaka moyoni mwake, amkamate, kwa kuwa njia ni ndefu, ampige, azimie roho, naye yule hakukora manza za kuuawa, kwani hakuwa mchukivu wake tangu zamani. Kwa sababu hii mimi ninakuagiza kwamba: Jitengee miji mitatu! Tena itakuwa, Bwana Mungu wako aipanue mipaka yako, kama alivyowaapia baba zako, ya kuwa atawapa. Hivi vitakuwa, ukiyaangalia na kuyafanya haya maagizo yote, mimi ninayokuagiza leo, umpende Bwana Mungu wako, uzishike njia zake siku zote; basi, hapo, hivyo vitakapotimia, sharti hiyo miji mitatu uiongeze kwa kujitengea mji mitatu mingine, ni kwamba: katikati ya hiyo nchi yako, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe fungu lako, isimwagwe damu ya mtu asiyekora manza za kufa, hiyo damu ikakukalia wewe. Lakini mtu akiwa mchukivu wa mwenzake, akamvizia na kumnyatianyatia, mwisho akampata, ampige na kuizimiza roho yake, afe kabisa; napo, atakapokimbilia miji hiyo mmojawapo, wazee wa mji wake na watume watu, wamchukue kule na kumtia mikononi mwake mlipiza hiyo damu, afe. Jicho lako lisimwonee machungu, upate kuondoa kwao Waisiraeli damu ya mtu asiyekora manza za kufa. Ndipo, utakapoona mema. Usimsogezee mwenzako mipaka, wakale waliyoikata penye fungu lako, utakalolichukua, liwe lako katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe yako. Mtu mmoja asimwondokee mwingine katika shauri la manza zo zote, wala la ukosaji wo wote uliomkosesha mtu kosa lo lote, watu wanalolikosa, ila shauri litawezekana tu kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. Shahidi mkorofi atakapomwinukia mwenzake kumsingizia upotovu, Nao watu wawili wanaobishana na waende kusimama mbele ya Bwana na mbele ya watambikaji na mbele ya waamuzi watakaokuwapo siku hizo, nao waamuzi na watafute vema sana iliyo kweli. Nao watakapoona, ya kama yule shahidi ni shahidi wa uwongo, naye alitaka kumkorofisha ndugu yake kwa uwongo, basi, na mmfanyie yaleyale, aliyoyawazia kumfanyizia ndugu yake. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako. Wao wengine wasiokuwapo watakapovisikia wataogopa, wasiendelee kufanya mambo mabaya kama hayo katikati yako. Jicho lako lisiwaonee machungu, ila uwatoze roho kwa roho, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu. Utakapotoka kwenda vitani kupigana na adui zako, ukaona farasi na magari na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope! Kwani Bwana Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri kukuleta huku yuko pamoja na wewe. Tena hapo, mapigano yatakapokuwa karibu, mtambikaji na awakaribie ninyi kusema na watu. Awaambie: Sikilizeni, Waisiraeli! Ninyi leo mnakwenda kupigana na adui zenu, lakini kwa hiyo mioyo yenu isilegee, msiwaogope na kutetemeka, wala msiwastuke. Kwani Bwana Mungu wenu atakwenda pamoja nanyi kuwapigania na adui zenu, awaokoe. Kisha wenye amri na waseme na watu na kuwaambia: Kama yuko mtu aliyejenga nyumba mpya, naye hajaieua, bado, na aende kurudi nyumbani kwake, asife katika mapigano, mtu mwingine akiieua. Au kama yuko mtu aliyepanda shamba la mizabibu naye hajalilimbua, na aende kurudi nyumbani kwake, asife katika mapigano, mtu mwingine akalilimbua. Au kama yuko mtu aliyeposa mwanamke, naye hajamwoa, na aende kurudi nyumbani kwake, asife katika mapigano, mwingine akamwoa. Kisha mwenye amri na aendelee kusema na watu na kuwaambia: kama yuko mtu mwoga mwenye moyo uliolegea, na aende kurudi nyumbani kwake, asiiyeyushe mioyo ya ndugu zake kuwa, kama moyo wake ulivyo. Nao wenye amri watakapokwisha kusema na watu, na waweke wakuu wa vikosi kuwatangulia watu. Utakapokaribia mji kupigana nao, kwanza uulize mapatano. Watakapokuitikia kwa kutaka mapatano, wakakufungulia malango, basi, watu wote watakaoonekana humo watakufanyizia kazi za nguvu na kukutumikia hivyo. Lakini watakapokataa kukuitikia mapatano wakitaka kupigana na wewe, basi, na uusonge. Bwana Mungu wako atakapoutia mikononi mwako, sharti uwapige wa kiume wote waliomo kwa ukali wa upanga. Lakini wanawake na watoto na nyama wa kufuga nayo yote yatakayokuwa humo mjini na ujitwalie yote pia kuwa mateka yako ya humo mjini, nawe utaweza kula mateka ya adui zako, Bwana Mungu wako atakayokupa. Hivyo ndivyo, utakavyoifanyizia miji yote iliyoko mbali sana kutoka kwako, isiyo miongoni mwa miji ya wamizimu hawa wa huku. Lakini katika miji ya haya makabila, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe fungu lako mwenyewe, usiponye hata mmoja avutaye pumzi. Ila sharti uwatie mwiko kabisa wa kuwapo hao Wahiti na Waamori na Wakanaani na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza, kusudi wasiwafundishe ninyi kuyafanya hayo matapisho yote, waliyoifanyizia miungu yao, ninyi mkamkosea Bwana Mungu wenu. Utakapokaa siku nyingi kwa kusonga mji na kupigana nao, upate kuuteka, usiiharibu miti yake na kuikata kwa shoka, ila ule matunda yao, kwa hiyo usiikate. Au miti ya shambani ni watu, uiendee kuisonga nayo usoni pako? Hiyo miti tu, utakayoijua, ya kuwa siyo miti izaayo matunda, na uiharibu na kuikata, uitumie ya kuujengea boma mji huo unaopigana na wewe, hata uanguke. Atakapoonekana mtu aliyeuawa katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe yako, naye akiwa analala porini, yule aliyemwua asijulikane, basi, wazee wako na waamuzi wako na watoke, wazipime njia za kwenda katika miji inayomzunguka yule mtu aliyeuawa. Wazee wa mji huo utakaokuwa karibu zaidi ya yule mtu aliyeuawa sharti wachukue mori ya ng'ombe asiyefanyishwa kazi bado, wala asiyevuta bado gari au jembe. Huyo mori wazee na wamtelemshe penye mto usiokupwa, pasipolimwa wala pasipopandwa, kisha wamvunje huyo mori shingo huko mtoni. Kisha watambikaji Walawi na waje huko, kwani Bwana Mungu wako aliwachagua kumtumikia na kubariki katika Jina lake Bwana, magomvi yote na mapigano yote yamalizwe kwa kusema kwao. Kisha wazee wote wa mji huo ulio karibu zaidi ya yule mtu aliyeuawa na wainawe mikono yao juu ya huyo mori aliyevunjwa shingo huko mtoni na kusema kwa kupaza sauti: Mikono yetu haikuimwaga damu hii, wala macho yetu hayakuona, ilipomwagwa. Bwana, wapoze walio ukoo wako wa Isiraeli, uliowakomboa, usiwalipishe damu ya mtu asiyekora manza iliyomwagwa katikati yao walio ukoo wako wa Isiraeli! Ndipo, watakapopata upozi kwa ajili ya hiyo damu. Hivyo ndivyo, utakavyoondoa katikati yako damu ya mtu asiyekora manza, utakapoyafanya haya yaongokayo machoni pake Bwana. Utakapotoka kwenda kupigana na adui zako, naye Bwana Mungu wako atakapowatia mikononi mwako, uwachukue kuwa mateka. Nawe ukiona katika hayo mateka mwanamke mwenye mwili mzuri wa kupendezwa naye, basi, utamchukua kuwa mkeo. Kwa hiyo umwingize nyumbani mwako, ajinyoe nywele za kichwani pake, ajikate nazo kucha za vidoleni pake, azivue nazo nguo, alizokuwa amezivaa alipotekwa, akae nyumbani mwako na kumwombolezea baba yake na mama yake mwezi mzima, kisha utaingia kwake, uwe mumewe, naye awe mkeo. Lakini itakapokuwa, usipendezwe tena naye, utampa ruhusa, ajiendee, atakakopenda, lakini usimwuze kwa fedha, wala usimkorofishe, kwa kuwa ulimtumia kuwa mkeo. Itakuwa, mtu awe na wake wawili, naye mmoja atapendezwa naye, lakini wa pili atachukizwa naye, wakamzalia watoto, yule apendezwaye naye naye yule achukizwaye naye, naye mwana wa kwanza ni wake yule achukizwaye naye. Baadaye siku zitakapotimia, awagawanyie wanawe mali zake, wazichukue, ziwe urithi wao, hataweza kumfanya mwanawe yule apendezwaye naye kuwa mwana wa kwanza mahali pake mwanawe wa kwanza aliyezaliwa naye yule achukizwaye naye, ila hana budi kumtokeza kuwa wa kwanza huyo mwana aliye wake mkewe achukizwaye naye, amgawie mafungu mawili ya mali zake zote zinazoonekana kwake, kwani huyo ni wa kwanza, nguvu zake ziliyemzaa; kwa hiyo haki ya kuzaliwa wa kwanza ni yake yeye. Itakuwa, mtu awe na mwana mtundu na mkatavu asiyesikia wala sauti ya baba yake wala sauti ya mama yake, asisikie, ijapo wamchape, basi, baba yake na mama yake na wamkamate, wampeleke kwao wazee wa mji wao langoni pake, wawaambie wazee: Huyu mwana wetu ni mtundu na mkatavu, hazisikii sauti zetu, ni mlafi na mnywaji. Kisha watu wote wa huo mji wa kwao na wamtupie mawe, afe. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako, kwani Waisiraeli wote watakapovisikia wataogopa. Itakuwa, mtu aliyekora manza za kufa auawe, watu wakimtundika mtini. Lakini mzoga wake usikae hapo mtini usiku kucha, ila sharti umzike siku iyo hiyo, kwani aliyetundikwa ameapizwa na Mungu; huko ni kwamba: usiipatie uchafu nchi hiyo, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe fungu lako mwenyewe. Utakapoona, ng'ombe au kondoo wa ndugu yako wakipotea, usijifiche kuwa kama mtu asiyewaona, ila sharti uwarudishe kwake ndugu yako. Kama huyo ndugu yako hakai karibu yako, usimjue, uwaweke nyumbani mwako, wakae kwako, mpaka ndugu yako awatafute; ndipo, utakapowarudisha kwake. Ndivyo ufanye hata utakapomwona punda wake au nguo zake au cho chote, ndugu yako atakachopotelewa nacho; wewe utakapokiona hutaweza kujificha kuwa kama mtu asiyeona. Utakapoona, punda wa ndugu yako au ng'ombe wake wakianguka njiani, usijifiche kuwa kama mtu asiyewaona, ila sharti umsaidie kuwainua. Mwanamke asivae cho chote cha mwanamume, wala mwanamume asivae nguo za kike! Kwani kila atakayefanya mambo kama hayo humchukiza Bwana Mungu wako. Utakapokuta kiota cha ndege njiani, kiko mbele yako katika mti au chini mchangani chenye makinda au chenye mayai, naye mama akiwaatamia makinda au mayai, usimchukue mama pamoja na watoto, ila umwache mama, ajiendee, uchukue watoto tu, upate kuona mema, nazo siku zako ziwe nyingi. Utakapojenga nyumba mpya, sharti juu darini utengeneze kikingio, usifanye nyumbani mwako kuwa mwenye damu ya mtu, mtu akianguka huko. Shamba lako la mizabibu usilipande mbegu za namna mbili, lote pia lisiwe mali ya Patakatifu: mbegu, ulizozipanda, pamoja na mazao ya mizabibu. Ukilima usitumie ng'ombe na punda pamoja. Usivae nguo iliyofumwa kwa kuchanganya nyuzi za manyoya ya kondoo na za pamba pamoja. Jifanyizie vishada penye pembe zote nne za nguo zako za kijifunika! Itakuwa, mtu amwoe mkewe na kuingia kwake, kisha achukizwe naye. Kwa hiyo atamsingizia mambo ya uwongo, ampatie jina baya na kusema: Nimemwoa mwanamke huyu; lakini nilipoingia kwake sikumwona kuwa mwanamwali. Vitakapokuwa hivyo, babake na mamake yule msichana na wamchukue na kumpeleka kwa wazee wa mji huo langoni pake pamoja nayo yanayoweza kuujulisha uwanawali wake. Naye babake yule msichana na awaambie wazee: Nimempa mwanangu mtu huyu kuwa mkewe, kisha akachukizwa naye; akamsingizia mambo ya uwongo kwamba: Sikumwona kuwa mwanamwali. Lakini yatazameni haya yanayoujulisha uwanawali wa mwanangu! Kisha waikunjue hiyo nguo mbele ya wazee wa mji huo. Kwa hiyo wazee wa mji huo na wamchukue yule mwanamume, wamchape. Kisha wamtoze fedha mia, wampe babake msichana, kwa kuwa yule alimpatia msichana wa Kiisiraeli jina baya; kisha awe mkewe, asiweze kumpa ruhusa kwenda zake siku zake zote. Lakini lile neno likiwa la kweli, nayo yanayoujulisha uwanawali wake yasipoonekana, na wampeleke yule msichana hapo pa kuiingilia nyumba ya baba yake, hapo watu wa mji wote wampige mawe, hata afe, kwa kuwa alifanya ujinga mbaya kwao Waisiraeli wa kufanya ugoni nyumbani mwa baba yake. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako. Mtu atakapooneka, ya kuwa amelala na mwanamke aliyeolewa na mwingine, sharti wafe wote wawili, yule mwanamume aliyelala na mwanamke, naye mwanamke. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo kwao Waisiraeli. Mwanamwali akiisha kuposwa na mtu, tena mwingine aliyemkuta mjini akilala naye, sharti mwapeleke wote wawili langoni pa mji huo, mwapige mawe, hata wafe, yule kijana wa kike, kwa kuwa hakupiga kelele mjini, naye yule mwanamume, kwa kuwa amemkorofisha mchumba wa mwenzake. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako. Lakini mwanamume atakapomkuta shambani kijana wa kike aliyekwisha kuposwa, akamkamata kwa nguvu, akalala naye, basi, huyu mwanamume aliyelala naye atakufa peke yake, lakini yule kijana wa kike msimfanyizie neno, kwani yule kijana wa kike hakukosa neno lipasalo, auawe, kwa kuwa jambo hili ni sawasawa, kama mtu aliyemwinukia mwenziwe na kumwua, afe. Kwani alimkuta shambani, naye yule kijana wa kike aliyekwisha kuposwa alipolia, hakuwako aliyemwokoa. Mtu atakapoona mwanamwali asiyeposwa bado, akamshika na kulala naye, basi, wakionwa, yule mwanamume aliyelala naye sharti ampe babake yule kijana wa kike fedha hamsini, kisha sharti awe mkewe, kwa kuwa amemkorofisha, naye hana ruhusa kumwacha siku zake zote. Mtu asimchukue mkewe baba yake, wala asiifunue pembe ya nguo zake! Katika mkutano wa Bwana asiingie mume aliyekomeshwa kuzaa kwa kupondwa au kwa kukatwa. Katika mkutano wa Bwana asiingie mwana wa ugoni wa ndugu na ndugu; ijapo awe wa kizazi chake cha kumi, asiingie katika mkutano wa Bwana. Mwamoni wala Mmoabu asiingie katika mkutano wa Bwana, ijapo awe wa kizazi chao cha kumi, kale na kale na wasiingie katika mkutano wa Bwana. Kwa kuwa hapo, mlipotoka Misri, hawakuwaendea na kuwapelekea ninyi wala chakula wala maji, tena walimkodisha Bileamu, mwanawe Beori, na kumtoa Petori ulioko Mesopotamia, aje, akuapize. Lakini Bwana Mungu wako akakataa kumsikia Bileamu, akakugeuzia kiapizo chake kuwa mbaraka kwa hivyo, Bwana Mungu wako alivyokupenda. Nawe usiwatafutie utengemano wala mema yo yote siku zako zote kale na kale! Lakini Mwedomu usichukizwe naye; kwani ni ndugu yako. Wala Mmisri usichukizwe naye, kwani ulikuwa mgeni katika nchi yake. Wana wao watakaozaliwa wa kizazi cha tatu wataweza kuingia katika mkutano wa Bwana. Utakapotoka makambini kuwaendea adui zako, jiangalie, usifanye kibaya cho chote! Atakapokuwako kwako mtu asiye mwenye kutakata kwa jambo lililompata na usiku, sharti atoke kwenda nje ya makambi, asiingie ndani ya makambi. Itakapokuwa saa ya jioni, ajiogeshe majini, kisha jua litakapokuchwa, aweza kuingia ndani ya makambi. Tena huko nje ya makambi uwe na mahali pa kuendea chooni. Namo katika vyombo vyako uwe na muo; napo utakapokwenda chooni huko nje, kwanza ufukue nao kishimo, upate kukaa, kisha uyafunike yaliyokutoka. Kwani Bwana Mungu wako hutembea katikati ya malango yako, akuponye na kuwatia adui zako mikononi mwako. Kwa hiyo makambi yako sharti yawe matakatifu, asione kwako cho chote kisichofaa, akarudi nyuma na kukuacha. Mtumwa aliyekukimbilia, ajiponye mikononi mwa bwana wake, usimrudishe kwake yule bwana wake. Na akae kwako mahali, atakapojichagulia po pote penye malango yako patakapokuwa pema machoni pake, nawe usimsumbue. Katika wana wa kike wa Kiisiraeli wasiwe wagoni wa Patakatifu, wala katika wana wa kiume wa Kiisiraeli wasiwe wagoni wa Patakatifu. Wala usiingize Nyumbani mwa Bwana Mungu wako mshahara wa ugoni wala fedha za kuuza mbwa, ijapo ziwe za kiapo cho chote, kwani Bwana Mungu wako huzikataa zote mbili kwa kuchukizwa nazo. Usimkopeshe ndugu yako, ujipatie faida ya fedha au faida ya chakula au faida ya cho chote, watu wanachokikopeshea faida. Asiye wa Kiisiraeli na umkopeshe, ujipatie faida, lakini ndugu yako usimkopeshe, ujipatie faida, kusudi Bwana Mungu wako akubarikie kazi zote, mikono yako itakazozifanya katika hiyo nchi, utakayoiingia kuichukua, iwe yako. Utakapoapa kiapo cha kumpa Bwana Mungu wako cho chote usikawie kukitimiza, kwani Bwana Mungu wako atakitafuta kwako, nawe usipompa utakuwa kama mwenye kujikosesha. Lakini utakapoacha kuapa hivyo hukosi. Lakini yaliyokwisha kutoka midomoni mwako sharti uyaangalie na kuyafanya, kama ulivyomwapia Bwana Mungu wako kwa kuyapenda mwenyewe uliyoyasema kwa kinywa chako. Utakapoingia mizabibuni kwa mwenzako utaweza kula zabibu, kama roho yako itakavyopenda, hata ushibe, lakini usitie nyingine chomboni. Utakapoingia penye ngano za mwenzako zilizoiva utaweza kukonyoa masuke kwa mkono wako, lakini usiyakatekate mabua ya mwenzako kwa mundu. Mtu akichukua mwanamke na kumwoa, naye halafu asipompendeza machoni pake, kwa kuwa ameona kwake neno lisilofaa, na amwandikie cheti cha kuachana na kumpa mkononi mwake, kisha na amtume kwenda zake na kutoka nyumbani mwake. Atakapokwisha kutoka nyumbani mwake, na aende zake kuwa mke wa mtu mwingine. Naye huyu mumewe wa pili atakapochukizwa naye, na amwandikie naye cheti cha kuachana na kumpa mkononi mwake, kisha naye na amtume kwenda zake na kutoka nyumbani mwake. Hata itakapokuwa, huyu mumewe wa pili aliyemchukua kuwa mkewe afe, bwana wake wa kwanza aliyemtuma kwenda kwao hana ruhusa kumchukua kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa uchafu, kwani haya humchukiza Bwana. Kwa hiyo usiikoseshe hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe fungu lako. Mtu akichukua mwanamke mpya asitoke kwenda vitani, wala asifanyishwe kazi yo yote nyingine, sharti mwaka mmoja aachwe tu kukaa nyumbani mwake, amfurahishe mkewe, aliyemchukua. Mtu usimtoze mawe ya kusagia, wala hilo la juu tu kuwa rehani, kwani hivyo ungemtoza yule mtu roho kuwa rehani. Atakapoonekana mtu atakayemwiba mwingine kwao wana wa Isiraeli, amtumie kuwa mtumwa au amwuze, mwizi huyu hana budi kuuawa; ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako. Jiangalie, utakapopatwa na pigo la ukoma! Yaangalie sana na kuyafanya yote sawasawa, kama watambikaji Walawi watakavyowafunza ninyi! Kama nilivyowaagiza wao, yaangalieni, myafanye vivyo hivyo! Yakumbuke, Bwana Mungu wako aliyomfanyizia Miriamu njiani, mlipotoka Misri. Utakapomkopesha mwenzako cho chote, alichokukopa, usiingie nyumbani mwake kumtoza roho yake, ila usimame nje, yule mtu uliyemkopesha wewe akutolee rehani yake huko nje. Naye kama ni mtu mnyonge, usilale na rehani yake, ila umrudishie rehani yake, jua litakapokuchwa, apate kulala na nguo yake ya kujifunika, akubariki. Hii itakupatia wongofu machoni pake Bwana Mungu wako. Usimkorofishe mtu wa kazi aliye mkiwa na mkosefu wa mali, kama ni wa ndugu zako au mmojawapo wa wageni watakaokaa katika nchi yako malangoni pako, ila umpe mshahara wake siku iyo hiyo, jua lisije kuchwa, akiwa hajapata, kwani ni mkiwa, huutaka sana wa kujitunza, asimlilie Bwana kwa ajili yako, ukawa mwenye kujikosesha. Baba asiuawe kwa ajili ya mwana, wala mwana asiuawe kwa ajili ya baba, ila kila mtu auawe kwa ajili ya kosa lake mwenyewe. Usipotoe shauri la mgeni wala la mwana aliyefiwa na wazazi, wala mjane usimtoze nguo yake kuwa rehani! Nawe kumbuka, ya kama ulikuwa mtumwa huko Misri, Bwana Mungu wako akakukomboa na kukutoa huko. Kwa sababu hii mimi ninakuagiza kuyafanya haya. Utakapoyavuna mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda mmoja shambani, usirudi kuuchukua, ila uache, uwe wa mgeni au wa mwana aliyefiwa na wazazi au wa mjane, Bwana Mungu wako akubarikie kazi zote za mikono yako. Utakapoupukutisha mchekele wako usiurudie tena kuyapukutisha nayo matawi yake, matunda yao na yawe ya mgeni au ya mwana aliyefiwa na wazazi au ya mjane. Utakapochuma mizabibuni kwako, usiirudie mizabibu kuiokoteza. Na iwe ya mgeni au ya mwana aliyefiwa na wazazi au ya mjane. Nawe kumbuka, ya kama ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri! Kwa sababu hii mimi ninakuagiza kuyafanya haya. Watu watakapogombana na waende shaurini, waamuliwe, mwamuzi akimtokeza asiyekosa kuwa hakukosa, naye aliyekosa kuwa amekosa. Huyo mkosaji akipaswa na kupigwa, mwamuzi na amlaze chini, wampige mbele yake fimbo zilizoyapasa maovu yake, nazo zihesabiwe. Wakiisha kumpiga 40 wasiendelee! Kwani wakiendelea kumpiga kuzipita hizo, mapigo yatazidi, naye ndugu yako atabezwa machoni pako. Ng'ombe mwenye kupura ngano usimfunge kinywa! Ndugu wakikaa pamoja, mmoja wao akafa pasipo kuacha mwana wa kiume, mkewe yule aliyekufa asiolewe nje na mtu mgeni, ila ndugu yake mumewe sharti amwingilie na kumchukua kuwa mkewe, amsimikie ndugu yake unyumba. Naye mwana wa kwanza, huyu mwanamke atakayemzaa, sharti amwandike kwa jina la ndugu yake aliyekufa, hilo jina lake lisifutwe kwao Waisiraeli. Lakini yule mtu asipopendezwa kumchukua mkewe ndugu yake, huyu mke wa ndugu yake na apande kwenda langoni kwa wazee, awaambie: Ndugu yake mume wangu amekataa kumwinulia ndugu yake jina kwao Waisiraeli, asipotaka kumsimikia unyumba kwa kunichukua. Kisha wazee wa mji huo na wamwite, waseme naye. Atakaposimama na kusema: Sipendezwi kumchukua, yule mkewe ndugu yake na amkaribie machoni pao wazee, amvue kiatu mguuni pake na kumtemea mate usoni, kisha na aseme kwamba: Mtu asiyeijenga nyumba ya ndugu yake na afanyiziwe hivyo! Kwa hiyo na aitwe jina lake kwao Waisiraeli: Nyumba ya mvuliwa kiatu. Watu wawili walio ndugu wakipigana, naye mkewe mmoja wao akaja kumponya mumewe mkononi mwake anayempiga, akaupeleka mkono wake na kumkamata penye soni, sharti umkate huo mkono wake pasipo kumwonea huruma. Mfukoni mwako usiwe na vyuma vya kupimia vya namna mbili, vikubwa na vidogo. Wala nyumbani mwako usiwe na pishi za namna mbili, kubwa na ndogo. Vyuma vyako vya kupimia sharti viwe vizima vilivyo sawasawa, nazo pishi zako ziwe nzima zilizo sawasawa, siku zako zipate kuwa nyingi katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa. Kwani Bwana Mungu wako huwachukia wanaoyafanya hayo yote, wao wote wafanyao mapotovu. Yakumbuke, Waamaleki waliyokufanyizia njiani, mlipotoka Misri! Walikushambulia njiani, wakawauwa wote waliokufuata nyuma kwa kuwa wanyonge, nawe ulikuwa umechoka, ukataka kuzimia roho, lakini wao hawakumwogopa Mungu. Kwa hiyo hapo, Bwana Mungu wako atakapokutulizia adui zako wote watakaokuzunguka pande zote katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe fungu lako mwenyewe, hapo sharti utoweshe ukumbusho wa Waamaleki chini ya mbingu; usivisahau! Utakapoingia katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe fungu lako, utakapoichukua na kukaa huko, sharti uchukue malimbuko ya mazao yote ya hiyo nchi, utakayoyatoa katika hiyo nchi yako, Bwana Mungu wako atakayokupa. Kisha uyaweke kikapuni, uende mahali pale, Bwana Mungu wako atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake. Utakapofika umwendee mtambikaji atakayekuwapo siku hizo, umwambie: Leo hivi ninamshuhudia Bwana Mungu wako, ya kama nimeingia katika hiyo nchi, Bwana aliyowaapia baba zetu kutupa sisi. Ndipo, mtambikaji atakapokichukua hicho kikapu mkononi mwako, akiweke mbele ya hapo pa kumtambikia Bwana Mungu wako. Kisha uanze kusema mbele ya Bwana Mungu wako kwamba: Baba yangu alikuwa Mshami mwenye kutangatanga, akashuka Misri, akakaa huko ugenini pamoja na watu wachache, akapata kuwa huko taifa kubwa yenye nguvu na watu wengi. Lakini Wamisri wakatufanyizia mabaya, wakatutesa na kutufanyisha kazi ngumu za utumwa. Ndipo, tulipomlilia Bwana, Mungu wa baba zetu, naye Bwana akazisikia sauti zetu, akayaona mateso yetu na masumbuko yetu na masongano yetu, Bwana akatutoa katika nchi ya Misri kwa kutoa nguvu za kiganja chake na kwa kuukunjua mkono wake na kwa mambo makuu yaliyostusha na kwa vielekezo na kwa vioja, akatuingiza mahali hapa, akatupa nchi hii, nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali. Sasa tazama, nimeleta malimbuko ya mazao ya nchi hii, wewe Bwana uliyonipa. Kisha yaweke mbele ya Bwana Mungu wako na kumwangukia Bwana Mungu wako. Ndivyo, utakavyoyafurahia mema yote, Bwana Mungu wako aliyokupa wewe na mlango wako, uyafurahie wewe pamoja na Mlawi na mgeni atakayekaa kwako. Katika mwaka wa tatu, ndio mwaka wa kutolea mafungu ya kumi, utakapokwisha kuyatoa mafungu ya kumi yote ya mapato yako, umpe Mlawi na mgeni na mwana aliyefiwa na wazazi na mjane, wayale malangoni pako, hata washibe. Kisha useme mbele ya Bwana Mungu wako: Nimeyaondoa nyumbani mwangu yaliyo matakatifu, nikampa Mlawi na mgeni na mwana aliyefiwa na wazazi na mjane, nikayafanya maagizo yako yote sawasawa, kama ulivyoniagiza, sikupita agizo lako lo lote, wala sikusahau mojawapo. Nilipolala tanga sikuyala hata kidogo, wala nilipokuwa mwenye uchafu sikuyaondoa hata kidogo, wala sikutoa mengine kumpa mwenzangu aliyefiwa, ila nimeisikia sauti ya Bwana Mungu wangu, nikayafanya yote, kama ulivyoniagiza. Chungulia toka mbinguni penye Kao lako takatifu, uwabariki walio ukoo wako wa Isiraeli nayo nchi hii, uliyotupa, kama ulivyowaapia baba zetu. Nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali. Leo hivi Bwana Mungu wako anakuagiza kufanya maongozi haya na maamuzi haya, uyaangalie, upate kuyafanya kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote. Nawe umesema leo, ya kama unamtaka Bwana, awe Mungu wako, ya kama unataka kuzishika njia zake na kuyaangalia maongozi yake na maagizo yake na maamuzi yake na kuisikia sauti yake. Naye Bwana amekuambia leo, ya kama anakutaka, uwe ukoo wake ulio wake mwenyewe, kama alivyokuagia, tena ya kama anakutaka, uyaangalie maagizo yake yote; tena ya kama anataka kukufanya kuwa mkuu kuliko mataifa yote, aliowafanya, upate matukuzo na jina la utukufu kuliko wao, ni kwamba: upate kuwa ukoo mtakatifu wa Bwana Mungu wako, kama alivyosema. Mose pamoja na wazee wa Waisiraeli wakawaagiza watu kwamba: Yaangalieni maagizo yote, mimi ninayowaagiza leo! Siku hiyo, mtakapouvuka Yordani kwenda katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, ujisimikie mawe makubwa na kuyapaka chokaa! Kisha uyaandike maneno yote ya Maonyo haya utakapokwisha kuvuka, kusudi upate kuingia katika nchi hiyo, Bwana Mungu wako atakayokupa. Nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali, kama Bwana Mungu wa baba zako alivyokuambia. Hapo mtakapouvuka Yordani yasimikeni mlimani kwa Ebali mawe haya, ninayowaagiza leo, kisha myapake chokaa! Kisha umjengee huko Bwana Mungu wako mahali pa kumtambikia, napo pajengwe kwa mawe yasiyochongwa kwa chuma cho chote. Hapo pa kumtambikia Bwana Mungu wako sharti upajenge kwa mawe yaliyo mazima, kisha umtolee Bwana Mungu wako juu yake ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima. Uchinje nazo ng'ombe za tambiko za shukrani, upate kula huko na kumfurahia Bwana Mungu wako. Nayo yale mawe uyaandike maneno yote ya haya Maonyo na kuyachora vema! Kisha Mose na watambikaji Walawi wakawaambia Waisiraeli wote kwamba: Nyamaza kimya, Isiraeli, upate kusikia! Leo hivi umepata kuwa ukoo wake Bwana Mungu wako. Kwa hiyo isikie sauti ya Bwana Mungu wako, uyafanye maagizo yake na maongozi yake, mimi ninayokuagiza leo! Siku hiyo Mose akawaagiza watu kwamba: Hawa na waende kusimama mlimani kwa Gerizimu na kuwabariki hawa watu, mtakapokwisha kuuvuka Yordani: Simeoni na Lawi na Yuda na Isakari na Yosefu na Benyamini. Nao hao na waende kusimama mlimani kwa Ebali na kuapiza: Rubeni na Gadi na Aseri na Zebuluni na Dani na Nafutali. Kisha Walawi na waanze kusema na kuwaambia watu wote wa Waisiraeli kwa kupaza sauti: Na awe ameapizwa mtu atakayefanya kinyago cha kuchonga au cha kuyeyusha na kuvisimamisha na kufichaficha! Kwani Bwana huchukizwa navyo, navyo ni kazi za mikono ya fundi. Nao watu wote na waitikie: Amin! Na awe ameapizwa atakayembeza baba yake na mama yake! Nao watu wote na waitikie: Amin! Na awe ameapizwa atakayeusogeza mpaka wa mwenzake! Nao watu wote na waitikie: Amin! Na awe ameapizwa atakayempoteza kipofu njiani! Nao watu wote na waitikie: Amin! Na awe ameapizwa atakayepotoa shauri la mgeni au la mwana aliyefiwa na wazazi au la mjane! Nao watu wote na waitikie: Amin! Na awe ameapizwa atakayelala na mkewe baba yake! Kwani huko atazifunua nguo za baba yake. Nao watu wote na waitikie: Amin! Na awe ameapizwa atakayelala na nyama wo wote! Nao watu wote na waitikie: Amin! Na awe ameapizwa atakayelala na umbu lake aliye binti baba yake au binti mama yake! Nao watu wote na waitikie: Amin! Na awe ameapizwa atakayelala na mkwewe! Nao watu wote na waitikie: Amin! Na awe ameapizwa atakayempiga mwenzake mahali panapojificha! Nao watu wote na waititike: Amin! Na awe ameapizwa atakayechukua mapenyezo, ampige mtu na kuimwaga damu yake asiyekosa! Nao watu wote na waitikie: Amin! Na awe ameapizwa asiyeyasimamisha maneno ya Maonyo haya na kuyafanya! Nao watu wote na waitikie: Amin! Utakapoisikia sauti ya Bwana Mungu wako, uyaangalie na kuyafanya maagizo yake yote, mimi ninayokuagiza leo, Bwana Mungu wako atakufanya kuwa mkuu kuliko mataifa yote ya huku nchini. Ndipo, zitakapokujia hizi mbaraka zote na kukupata, utakapoisikia sauti ya Bwana Mungu wako. Utakuwa umebarikiwa mjini, nako shambani utakuwa umebarikiwa. Yatakuwa yamebarikiwa mazao ya tumbo lako na mazao ya nchi yako na mazao ya nyama wako wa kufuga na ndama wako na wana kondoo wako. Litakuwa limebarikiwa nalo kapu lako na bakuli lako la kutengenezea mikate. Utakuwa umebarikiwa wewe utakapoingia, tena utakuwa umebarikiwa wewe utakapotoka. Adui zako watakapokuinukia, Bwana atawatoa, wapigwe mbele yako: kwa njia moja watatoka kukuendea, lakini kwa njia saba watakukimbia. Bwana atakuagizia mbaraka, uipate chanjani mwako na katika kazi zote za mikono yako, maana atakubariki katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa. Bwana atakuweka kuwa ukoo wake mtakatifu, kama alivyokuapia, utakapoyaangalia maagizo yake Bwana Mungu wako na kuzishika njia zake. Ndipo, makabila yote ya huku nchini yatakapoona, ya kuwa umeitwa kwa Jina la Bwana, kisha watakuogopa. Naye Bwana atakufurikishia mema: mazao ya tumbo lako na mazao ya nyama wako wa kufuga na mazao ya mashamba yako katika hiyo nchi, Bwana aliyowaapia baba zako kukupa wewe. Nayo malimbiko yake mema ya mbinguni Bwana atakufunulia, ainyeshee nchi yako mvua, siku zake zitakapotimia, azibariki kazi zote za mikono yako, upate kukopesha mataifa mengi, lakini wewe hutakopa kabisa. Yeye Bwana atakufanya kuwa kichwa, usiwe mkia, upate kuwa juu tu, usilale chini ya wengine, utakapoyasikia maagizo ya Bwana Mungu wako, mimi ninayokuagiza leo kuyaangalia na kuyafanya. Haya maneno yote, mimi ninayokuagiza leo, usiyaache na kujiendea wala kuumeni wala kushotoni kwa kufuata miungu mingine na kuitumikia. Lakini usipoisikia sauti ya Bwana Mungu wako, usiyaangalie na kuyafanya maagizo yake yote na maongozi yake yote, mimi ninayokuagiza leo, ndipo, yatakapokujia haya maapizo yote na kukupata. Utakuwa umeapizwa mjini, nako shambani utakuwa umeapizwa. Litakuwa limeapizwa kapu lako nalo bakuli lako la kutengenezea mikate. Yatakuwa yameapizwa mazao ya tumbo lako na mazao ya nchi yako na ndama wako na wana kondoo wako. Utakuwa umeapizwa wewe utakapoingia, tena utakuwa umeapizwa wewe utakapotoka. Bwana atatuma kwako maapizo na mahangaiko na matisho katika kazi zote, mikono yako itakazozifanya, mpaka uangamizwe kwa kupotea upesi kwa ajili ya ubaya wa matendo yako, kwa kuwa umeniacha. Bwana atakugandamanisha na magonjwa ya moyo, mpaka amalize kukuondoa katika hiyo nchi, utakayoiingia kuichukua, iwe yako. Bwana atakupiga kwa kifua kikuu na kwa homa na kwa kidingapopo na kwa kipindu na kwa upanga na kwa jua kali na kwa kunyausha ngano; haya yatakuhangaisha wewe, hata uangamie. Nayo mbingu iliyoko juu yako itakuwa kama shaba, nayo nchi iliyoko chini yako itakuwa kama chuma. Mvua ya nchi yako Bwana ataigeuza kuwa vumbi na mchanga mwembamba, ikuguie toka mbinguni, hata uangamizwe. Bwana atakutoa, upigwe mbele ya adui zako: utatoka kwa njia moja kuwaendea, lakini utawakimbia kwa njia saba, kisha utatupwa huko na huko katika nchi zote zenye wafalme. Mzoga wako utaliwa na ndege wote wa angani na nyama wa huku nchini, nao hawataona atakayewaamia. Bwana atakupiga kwa matende ya Misri na kwa majipu mabaya na kwa buba na kwa upele usiowezekana kuponywa. Bwana atakupiga kwa kichaa na kwa upofu na kwa bumbuazi la moyo. Nawe utakuwa ukipapasapapasa na mchana, kama kipofu anavyopapasa gizani, lakini hutafanikiwa katika njia zako, utakaa siku zote ukikorofishwa na kunyang'anywa pasipo kuona mwokozi. Utakapoposa mke, mwingine atalala naye; utakapojenga nyumba hutakaa humo; utakapopanda mizabibu hutayala matunda yao. Ng'ombe wako atakapochinjwa machoni pako, hutaila nyama yake; punda wako atakapopokonywa machoni pako hatarudi kwako; adui zako watakapopewa mbuzi na kondoo wako, hutaona mwokozi. Watu wa kabila jingine watakapopewa wanao wa kiume na wa kike, macho yako yataviona na kuzimia kwa kuwatunukia mchana kutwa, lakini hakuna, mkono wako utakachoweza kukifanya. Mazao ya nchi yako nayo yote, uliyoyasumbukia, yataliwa na watu wageni, usiowajua, nawe utakaa tu kwa kukorofishwa na kupondwa siku zote. Nawe utakuwa mwenye wazimu kwa kuyaona hayo kwa roho yako, utakayoyaona. Bwana atakupiga kwa matende magotini na mapajani yasiyowezekana kuponywa, yakutokee toka wayo wa mguu wako mpaka utosini. Bwana atakupeleka wewe pamoja na mfalme wako, utakayejiwekea, kwa taifa, usilolijua wala wewe wala baba zako; huko utatumikia miungu mingine iliyo miti na mawe tu. Ndipo, utakapozomewa kwa mafumbo na kwa masimango katika makabila yote, ambayo Bwana atakakupeleka kwao. Mbegu nyingi utatoa nyumbani kupanda shambani, lakini utavuna machache tu, kwani nzige watazila. Utapanda mizabibu na kuilimia vema, lakini hutakunywa mvinyo, wala hutaichuma, kwani vimatu wataila. Utakuwa na michekele katika mipaka yako yote, lakini hutajipaka mafuta, kwani michekele yako itapukutisha mapooza tu. Utazaa wana wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa wako, kwa kuwa watatekwa. Miti yako yote nayo mazao ya nchi yako yatakuwa yao mabumundu. Mgeni atakayekuwa katikati yako atapaa juu zaidi, hata awe mkuu wako, lakini wewe utashuka kuwa chini zaidi. Yeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha; yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia. Haya maapizo yote yatakujia, yakuhangaishe; lakini yatakupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikia sauti ya Bwana Mungu wako na kuyaangalia maagizo yake na maongozi yake, aliyokuagiza. Kwa hiyo haya maapizo yatakuwa kielekezo na kioja kwako wewe nako kwao walio wa uzao wako kale na kale. Kwa kuwa hukumtumikia Bwana Mungu wako kwa furaha na kwa moyo wa kumshukuru kwa hivyo, alivyokufurikishia vyote, kwa sababu hii utawatumikia adui zako, Bwana atakaowatuma kwako, nawe utakuwa mwenye njaa na kiu, mwenye uchi na ukosefu wote, kisha atakutia kongwa la chuma shingoni pako, hata akuangamize. Bwana atakuletea taifa, atakalolitoa mbali kwenye mapeo ya nchi, warukao kama tai, usiowasikia msemo wao. Ndio watu wenye ukali usoni, hawautazami uso wa mzee, wala hawamhurumii kijana. Wao ndio watakaoyala mazao ya nyama wako wa kufuga nayo mazao ya mashamba yako, hata uangamizwe; maana hawatakusazia wala ngano wala mvinyo mbichi wala mafuta wala ndama wako wala wana kondoo wako, hata wakuangamize kabisa. Nao watakusonga malangoni pako pote, hata ziangushwe hizo kuta ndefu zenye nguvu za maboma yako, unazozijetea katika nchi yako yote; ndipo, utakaposongeka malangoni pako pote katika nchi yako yote, Bwana Mungu wako atakayokupa. Nawe kwa kusongeka na kwa kuhangaika utayala mazao ya tumbo lako, maana nyama zao wanao wa kiume na wa kike, Bwana Mungu wako atakaokupa; itakuwa hapo, adui zako watakapokuhangaisha. Ndipo, nayo macho yake mtu mwanana wa kwenu aliyejizoeza kula vya urembo tu yatakapokuwa mabaya, atakapowaona ndugu zake na mkewe wa kifuani pake na wanawe waliosalia, aliowasaza bado; kwani ataona choyo cha kuwagawia mmoja wao tu nyama za wanawe, anazozila, kwani atakuwa hanacho cho chote, alichojisazia kwa kusongeka na kwa kuhangaika, adui zako watakapokuhangaisha malangoni pako pote. Naye mwanamke mwanana wa kwenu aliyejizoeza kula vya urembo tu, asiyejaribu kale kuikanyaga nchi kwa wayo wa mguu wake, kwani alijizoeza kutumia vitu vya urembo tu kwa kuwa mwanana, basi, ndipo, macho yake nayo yatakapokuwa mabaya, atakapomwona mumewe wa kifuani pake na mwanawe wa kiume naye wa kike; maana atataka kuwanyima hata kondo ya nyuma iliyotoka katikati ya miguu yake na nyama za wanawe, aliowazaa, kwani anataka kuzila fichoni kwa kukosa chakula chote; haya atayafanya kwa kusongeka na kwa kuhangaika, adui zako watakapokuhangaisha malangoni pako. Usipoyaangalia na kuyafanya maneno yote ya Maonyo haya yaliyoandikwa humu kitabuni, upate kuliogopa hilo Jina tukufu litishalo la Bwana Mungu wako, Bwana atakupiga wewe nao wa uzao wako hayo mapigo ya kustaajabisha, nayo yatakuwa mapigo makubwa yatakayokaa sana, tena magonjwa mabaya yatakayokaa sana nayo. Atakurudishia maradhi yote ya Misri, uliyoyastuka, nayo yatagandamana na wewe. Nayo magonjwa yote na mapigo yote yasiyoandikwa katika kitabu cha Maonyo haya Bwana atakupatia, hata uangamizwe. Mtasazwa waume wachache tu, ninyi mliokuwa wengi kama nyota za mbinguni, kwa kuwa hukuisikia sauti ya Bwana Mungu wako. Kama Bwana alivyofurahia kuwafanyizia mema na kuwafanya kuwa wengi, ndivyo, Bwana atakavyofurahia kuwapoteza ninyi na kuwaangamiza, mng'olewe katika hiyo nchi, wewe unakokwenda sasa kuichukua, iwe yako. Kisha Bwana atakutawanya katika makabila yote toka mapeo ya nchi ya huku kuyafikia mapeo ya nchi ya huko, nako ndiko, utakakotumikia miungu mingine, usiyoijua wewe wala baba zako, iliyo miti na mawe tu. Lakini hutapata kutulia kwao wamizimu hao, wala wayo wa mguu wako hautaona kituo, kwani Bwana atakupa moyo utakaotapatapa tu, nayo macho yatakayopenda kuzimia tu, nayo roho itakayotunukia kukatika tu. Kwani uzima wako utakuwa, kama umening'inishwa kwa uzi mbele yako, kwa hiyo utakaa kiwogawoga usiku na mchana, kwa kuwa hutayategemea, ya kama utakaa uzimani. Asubuhi utasema: Laiti iwe jioni! napo jioni utasema: Laiti iwe asubuhi! Kwani moyo wako utakaa kiwogawoga kwa ajili ya hayo, utakayoyaogopa, na kuyaona yale mambo, macho yako yatakayoyaona. Kisha Bwana atakurudisha Misri kwa merikebu, uishike ile njia, niliyokuambia: Hutaiona tena. Huko mtauzwa kwa adui zenu kuwa watumwa na vijakazi, lakini hatakuwako atakayewanunua. Haya ndiyo maneno ya Agano, Bwana aliyomwagiza Mose kulifanya na wana wa Isiraeli katika nchi ya Moabu, tena liko Agano lile, alilolifanya nao mlimani kwa Horebu. Mose akawaita Waisiraeli wote, akawaambia: Ninyi mliona yote, Bwana aliyomfanyizia Farao, nao watumishi wake wote na wenyeji wote wa nchi yake machoni penu katika nchi ya Misri. Yale majaribu makubwa macho yako yaliyaona kuwa vielekezo na vioja vikubwa. Lakini mpaka siku hii ya leo Bwana hajawapa ninyi mioyo inayovitambua, wala macho yanayoona, wala masikio yanayosikia. Nayo hiyo miaka 40, niliyowatembeza nyikani, nguo zenu hazikuchakaa miilini penu, wala viatu vyako havikuchakaa miguuni pako; hamkula mikate, wala hamkunywa mvinyo au kileo kingine, mpate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu wenu. Mlipofika mahali hapa, Sihoni, mfalme wa Hesiboni, na Ogi, mfalme wa Basani, walitaka kupigana na sisi, nasi tukawapiga, tukazichukua nchi zao, tukawapa wao Warubeni na Wagadi nao wa nusu la shina la Manase, ziwe mafungu yao. Sasa yaangalieni maneno ya Agano hili na kuyafanya, mpate kufanikiwa mambo yote, mtakayoyafanya. Leo mnasimama nyote mbele ya Bwana Mungu wenu, walio vichwa vyenu vya mashina yenu, wazee wenu na wakuu wenu, nanyi nyote mlio waume wa Kiisiraeli, wana wenu na wake zenu na mgeni wako aliye makambini mwako naye mchanja kuni zako naye mchota maji yako. Huku ni kwamba, upate kuandamana nalo Agano la Bwana Mungu wako, analolifanya leo na wewe, nacho kiapo chake. Naye anakuweka leo kuwa ukoo wake, naye atakuwa Mungu wako, kama alivyokuambia, kama alivyowaapia nao baba zako Aburahamu na Isaka na Yakobo. Lakini si ninyi peke yenu, ninaofanya nao Agano hili na kuwaapia kiapo hiki, ila ni wao wanaosimama leo hapa pamoja na sisi mbele ya Bwana Mungu wetu, tena ni wao nao wasiokuwapo leo hapa pamoja na sisi. Kwani ninyi mnajua wenyewe, jinsi tulivyokaa katika nchi ya Misri, tena tulivyopita katikati ya wamizimu, ambao mlipita kwao, mkayaona matapisho yao na vinyago vyao, walivyokuwa navyo, vilivyo miti tu na mawe au fedha na dhahabu. Lakini kwenu asiwe mtu mume wala mke wala mlango wala shina watakaoigeuza mioyo yao, wamwache Bwana Mungu wetu wakienda kuitumikia miungu ya hao wamizimu, lisichipuke kwenu shina litakalozaa majani yenye sumu na uchungu kama wa nyongo. Mtu aliye hivyo atakapoyasikia maneno ya kiapizo hiki asijibariki mwenyewe moyoni mwake kwamba: Nitapata kutengemana, ijapo niendelee kuufuata ushupavu wa moyo wangu, kusudi niyapokonye mabichi na makavu. Aliye hivyo Bwana atakataa kabisa kumwondolea mabaya, ila hapo ndipo, makali ya Bwana pamoja na wivu wake yatakapowaka moto wenye moshi kwa kumkasirikia huyo mtu, navyo viapizo vyote vilivyoandikwa humu kitabuni vitamkalia, naye Bwana atalifuta jina lake chini ya mbingu. Tena Bwana atamtenga na kumtoa katika mashina yote ya Isiraeli, apatwe na mabaya, vimtimilikie viapizo vyote vya Agano hili lililoandikwa katika kitabu cha Maonyo haya. Navyo vizazi vijavyo nyuma, ndio wana wenu watakaotokea nyuma yenu, nao wageni watakaotoka katika nchi ya mbali watayaona hayo mapigo ya nchi hii nayo magonjwa, Bwana aliyoiuguza; kwani nchi yake nzima ataiteketeza kwa mawe ya kiberiti na kwa chumvi, isiweze kupandwa wala kuotesha kijiti, wala majani yo yote yasiweze kumea huko, mwangamizo wake uwe kama ule wa Sodomu na wa Gomora, nao wa Adima na wa Seboimu, Bwana aliyoiangamiza kwa makali yake yaliyowaka moto. Watakapoviona wamizimu wote watauliza: Bwana akiifanyizia nchi hii mambo kama haya, ni kwa sababu gani? Makali makuu yawakayo moto hivyo yako na maana gani? Ndipo, watu watakapowaambia: Ni kwa kuwa waliliacha Agano la Bwana Mungu wa baba zao, alilolifanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri; wakaenda zao, wakatumikia miungu mingine na kuitambikia, nayo ni miungu, wasiyoijua, isiyowagawia kitu. Ndipo, makali ya Bwana yalipoiwakia nchi hii, akailetea viapizo vyote vilivyoandikwa humu kitabuni. Bwana akawang'oa katika nchi yao kwa makali yaliyowaka moto na kwa machafuko makubwa, akawatupa, wajiendee katika nchi nyingine, kama inavyoelekea leo. Mambo yaliyofunikwa ni yake Bwana Mungu wenu; lakini yaliyofunuliwa ni yetu sisi na ya wana wetu, tuyafanye maneno yote ya Maonyo haya. Hayo yote yatakapokujia, hayo ya mbaraka nayo ya kiapizo, niliyoyaweka mbele yako, nawe utakapoyaingiza moyoni mwako katika wamizimu wote, Bwana Mungu wako atakapokukumba kwenda kwao, napo utakaporudi kwa Bwana Mungu wako, uisikie sauti yake na kuyafuata yote, mimi ninayokuagiza leo, uyafanye wewe na wanao kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote, ndipo, Bwana Mungu wako atakapoyafungua mafungo yako kwa kukuhurumia, akukutanishe tena na kukutoa katika makabila yote, Bwana Mungu wako alikokutawanya. Ijapo, uwe umekumbwa kwenda hata mapeoni kwa mbingu, huko nako Bwana Mungu wako atakukusanya na kukuchukua huko, Bwana Mungu wako akupeleke katika nchi, baba zako waliyoichukua, iwe yao, uichukue nawe, iwe yako, kisha atakukalisha vema na kukufanya kuwa wengi kuliko baba zako. Naye Bwana Mungu wako atautahiri moyo wako nayo mioyo yao wa uzao wako, mmpende Bwana Mungu wenu kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote, mpate kupona. Kisha Bwana Mungu wako atavitimiza hivyo viapizo vyote, viwapate adui zako na wachukivu wako waliokufukuza. Lakini wewe utaisikia tena sauti ya Bwana, uyafanye maagizo yake yote, mimi ninayokuagiza leo. Ndipo, Bwana Mungu wako atakapokupatia mema mengi ya kuyasaza katika kazi zote za mikono yako na katika mazao ya tumbo lako na katika mazao ya nyama wako wa kufuga na katika mazao ya mashamba yako, kwani Bwana atakufurahia tena, akupatie mema, kama alivyowafurahia baba zako. Hayo utayapata utakapoisikia sauti ya Bwana Mungu wako, uyaangalie magizo na maongozi yake yaliyoandikwa katika kitabu cha Maonyo haya, utakapomrudia Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote. Kwani hili agizo, mimi ninalokuagiza leo, silo gumu, usiweze kulifanya, wala haliko mbali, usiweze kulifikia: haliko mbinguni, useme: Yuko nani atakayetupandia mbinguni kulichukua na kutuletea, tulisikie, tupate kulifanya? Wala haliko ng'ambo ya bahari, useme: Yuko nani atakayetuvukia bahari kwenda ng'ambo ya huko kulichukua na kutuletea, tulisikie, tupate kulifanya? Kwani neno hilo linakukalia karibu sana, limo kinywani mwako namo moyoni mwako, upate kulifanya. Tazama, nimeweka leo mbele yako maisha na mema, tena kifo na mabaya. Mimi ninakuagiza leo kumpenda Bwana Mungu wako na kuzishika njia zake na kuyaangalia maagizo yake na maongozi yake na maamuzi yake, ndipo, utakapopona, watu wako wawe wengi, naye Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi hiyo, wewe unayokwenda kuichukia, iwe yako. Lakini moyo wako utakapogeuka, usisikie, utadanganyika, utambikie miungu mingine na kuitumikia. Nami ninawatangazia leo hivi: Mtaangamia kabisa, msikae siku nyingi katika hiyo nchi, unayouvukia Yordani, uiingie na kuichukua, iwe yako. Ninawatajia leo hivi mbingu na nchi kuwa mashahidi, ya kuwa nimeweka mbele yako maisha na kifo, mbaraka na kiapizo, ukayachagua maisha, upate kuishi wewe nao wa uzao wako, mkimpenda Bwana Mungu wenu, mwisikie sauti yake na kugandamana naye; kwani humu ndimo, yalimo maisha yako na wingi wa siku zako za kukaa katika hiyo nchi, Bwana aliyowaapia baba zako Aburahamu na Isaka na Yakobo kuwapa. Mose akaenda, akawaambia Waisiraeli wote maneno haya, akawaambia: Mimi leo ni mwenye miaka 120, siwezi tena kuingia na kutoka, naye Bwana aliniambia: Hutauvuka huu Yordani. Bwana Mungu wako atakutangulia mwenyewe, ukivuka; naye ndiye atakayeyaangamiza mataifa hayo mbele yako, upate kuzichukua nchi zao. Naye Yosua ndiye atakayekuvukisha, kama Bwana alivyosema. Naye Bwana atawafanyizia, kama alivyowafanyizia Sihoni na Ogi, wale wafalme wa Waamori, na wenyeji wa nchi zao, aliowaangamiza. Bwana atawatoa mbele yenu, mwafanyizie na kulifuata agizo, nililowaagiza ninyi. Jipeni mioyo, mpate nguvu, msiwaogope, wala msiwastuke! Kwani Bwana Mungu wako atakwenda pamoja na wewe, hataondoka kwako, wala hatakuacha. Kisha Mose akamwita Yosua, akamwambia machoni pao Waisiraeli wote: Jipe moyo, upate nguvu! Kwani wewe utaingia na watu hawa katika nchi hiyo, Bwana aliyowaapia baba zao kuwapa, kisha utawagawia mafungu yao ya nchi. Naye Bwana mwenyewe atakutangulia, awe pamoja na wewe; hataondoka kwako, wala hatakuacha; usiogope, wala usiingiwe na vituko! Mose akayaandika Maonyo haya, akawapa watambikaji, wana wa Lawi waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana, na wazee wote wa Waisiraeli. Kisha Mose akawaagiza kwamba: Kila miaka saba itakapopita, mwaka wa kuachilia madeni utakapotimia, penye sikukuu ya Vibanda, Waisiraeli wote watakapokuja kumtokea Bwana Mungu wako mahali pale, atakapopachagua, ndipo, utakapoyasoma Maonyo haya masikioni pao Waisiraeli wote. Hapo uwakutanishe watu wote, waume na wake na wana na wageni watakaokuwako malangoni pako, wayasikie, wapate kujifunza, wamwogope Bwana Mungu wenu, wayaangalie na kuyafanya maneno yote ya Maonyo haya. Nao wana wao wasioyajua na wayasikie, wapate kujifunza, wamwogope Bwana Mungu wenu siku zote, mtakazokuwako katika hiyo nchi, mnayoivukia Yordani, mpate kuichukua, iwe yenu. Bwana akamwambia Mose: Tazama, siku zako zimetimia, upate kufa! Mwite Yosua, mwende kusimama Hemani mwa Mkutano, nipate kumwagiza kazi. Ndipo, Mose na Yosua walipokwenda kusimama Hemani mwa Mkutano. Bwana akatokea mle Hemani katika wingu lililokuwa kama nguzo, nalo hilo wingu lililokuwa kama nguzo likasimama hapo pa kuliingilia Hema. Bwana akamwambia Mose: Tazama, unakwenda kulala na baba zako. Kisha watu wataondoka kwenda kufanya ugoni wa kufuata miungu migeni ya nchi hiyo, watakayoiingia, lakini mimi wataniacha na kulivunja Agano, nililolifanya nao. Siku hiyo makali yangu yatawawakia, nami nitawaacha na kuuficha uso wangu, wasiuone; kisha wataliwa na kupatwa na mabaya mengi ya kuwasonga. Siku hiyo watasema: Kumbe haya mabaya hayakutupata, kwa kuwa Mungu wetu hayumo katikati yetu? Lakini mimi nitauficha uso wangu kabisa siku hiyo kwa ajili ya mabaya yote, waliyoyafanya walipoigeukia hiyo miungu mingine. Sasa jiandikieni wimbo huu, mwafundishe wana wa Isiraeli na kuutia vinywani mwao, kusudi wimbo huu uwe shahidi wangu kwao wana wa Isiraeli! Kwani nitawaingiza katika hiyo nchi, niliyowaapia baba zao, ichuruzikayo maziwa na asali. Lakini watakapokula na kushiba na kunenepa, ndipo, watakapogeukia miungu mingine, waitumikie na kunibeza mimi na kulivunja Agano langu. Kisha hapo, mabaya mengi ya kuwasonga yatakapowapata, wimbo huu na uwajibu na kuwashuhudia, kwani hautasahauliwa vinywani mwao walio uzao wako. Kwani ninayajua mawazo yao, wanayoyatunga leo, kwa kuwa sijawaingiza bado katika hiyo nchi, niliyowaapia. Siku iyo hiyo Mose akauandika wimbo huo, akawafundisha wana wa Isiraeli kuuimba. Naye Yosua, mwana wa Nuni, Bwana akamwagiza kwamba: Jipe moyo, upate nguvu! Kwani wewe utawaingiza wana wa Isiraeli katika hiyo nchi, niliyowaapia; nami nitakuwa pamoja na wewe. Mose alipokwisha kuyaandika maneno ya Maonyo haya katika kitabu na kuyamaliza yote, Mose akawaagiza Walawi waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana kwamba: Kichukueni kitabu cha Maonyo haya, mkiweke kando ndani ya Sanduku la Agano la Bwana Mungu wenu, kiwe humo ndani shahidi wako! Kwani ninaujua ukatavu wako na ugumu wa ukosi wako; tazameni, siku hizi za leo, ninapokuwa bado mwenye uzima pamoja nanyi, mmekuwa wenye kumkataa Bwana. Tena itakuwaje, nitakapokwisha kufa? Wakusanyeni mbele yangu wazee wote wa mashina yenu na wakuu wenu, niyaseme masikioni pao hayo maneno ya kuwatajia mbingu na nchi kuwa mashahidi. Kwani ninajua, ya kama hapo, nitakapokwisha kufa, mtafanya mabaya sana mkiondoka katika njia, niliyowaagiza; kwa hiyo ubaya utawapata siku za mwisho, kwani mtayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bana, mmkasirishe kwa kazi za mikono yenu. Kisha Mose akayasema maneno ya wimbo huu masikioni pao wa mkutano wote wa Waisiraeli na kuyamaliza yote. Yasikilizeni, ninyi mbingu, nitakayoyasema! Nawe nchi, yasikilize maneno ya kinywa changu! Mafunzo yangu na yatiririke kama maji ya mvua, maneno yangu na yadondoke kama umande,, kama manyunyu yanayonyunyiziwa majani mabichi, kama matone ya mvua yanayotonea vijiti! Kwani nitalitangaza Jina la Bwana, nanyi mpeni ukuu aliye Mungu wetu! Ni mwamba, matendo yake humalizika, kwani njia zake zote huendelea sawa, ni Mungu mtegemevu asiye na upotovu, ni mwenye wongofu, tena ni mnyofu. Wasio watoto wake kwa kuwa wachafu, humfanyia mabaya, ndio kizazi chenye upotovu, hupenda kubisha. Mbona mnamlipa Bwana hivyo? M wapumbavu wasiojua maana? Kumbe siye baba yako aliyekununua? Siye aliyekufanya na kukutengeneza vema? Zikumbuke siku za kale, uitambue miaka yao vizazi vilivyopita! Mwulize baba yako! Atakusimulia; waulize wazee! Nao watakuambia. Alioko huko juu alipoyagawia mataifa mafungu yao ya nchi, alipowatawanya wana wa watu, ndipo, alipoiweka mipaka ya makabila kwa hesabu yao wana wa Isiraeli. Kwani fungu lake Bwana ni huu ukoo wake, aliojipatia kwa kura kuwa wake, ndio wa Yakobo. Alimwona katika nchi ya nyikani isiyo ya watu, nayo ilikuwa inatisha kwa ngurumo za nyama wa jangwani, akamkingia pande zote na kumjengea; kama ni mboni ya jicho lake, ndivyo, alivyomlinda. Alikuwa kama tai akitaka kuwainua hao wanawe kiotani na kupapatika juu yao hayo makinda yake; ndivyo, alivyoyakunjua mabawa yake, amchukue, ndivyo, alivyompeleka, akizikalia mbawa zake. Yeye Bwana peke yake ndiye aliyemwongoza, mungu mwingine wa ugenini hakuwa naye. Akampitisha juu ya nchi akimlisha mazao ya mashambani, akamnyonyesha asali ya ngomeni na mafuta ya mwambani na siagi za ng'ombe na maziwa ya kondoo, nayo mafuta yao wana kondoo, nayo ya madume ya kondoo wa Basani, nayo ya madume ya mbuzi, nayo mafuta menginemengine kama ya kiini cha ngano, ukanywa nazo mvinyo nyekundu zilizo damu za zabibu. Lakini Yeshuruni* aliponona akapiga mateke kwa kunona na kunenepa na kwa kushiba sana; ndipo, yeye alipomtupa Mungu, naye ndiye aliyemfanya; akambeza yule aliyekuwa mwamba wa wokovu wake. Kwa kufuata miungu migeni wakamchokoza, kwa kufanya yaliyomchukiza wakamkasirisha. Ng'ombe za tambiko wakaitolea nayo mizimu isiyo Mungu, hata miungu mingine, wasiyoijua; kwa kuzushwa siku hizo za karibu ilikuwa mipya, nao baba zenu walikuwa hawakuipa macheo. Aliyekuzaa ukamwazia kuwa si kitu, naye ni mwamba; ukamsahau Mungu, ambaye ulizaliwa naye. Bwana alipoyaona akawatupa kwa kuwakasirikia wanawe wa kiume na wa kike. Akasema: Na niufiche uso wangu, wasiuone, mimi niuone mwisho wao, jinsi utakavyokuwa, kwani ndio kizazi chenye mapotovu, ndio wana wasiotegemeka. wamenichokoza kwa kufuata isiyo miungu, wakanikasirisha kwa kufanya yasiyo na maana, kwa hiyo nami na niwachokoze nikiwaletea watu wasio watu, na niwakasirishe nikiwaletea taifa la watu wasiojua maana. Kwani uko moto uliowashwa na makali yangu, nao ukachoma na kufika hata kuzimuni kuliko chini ya nchi, ukaila nchi na mazao yake, nayo misingi ya milima ukaiunguza. Nitawapatia mabaya mengi, yawe chungu zima, nitaimaliza mishale yangu kwa kuwapiga. Itakapokuwa, wazimie roho kwa njaa tu, tena itakapokuwa, waliwe na moto ulio wa homa kali, itakapokuwa, wapatwe na magonjwa yenye uchungu, ndipo, nitakapotuma kwao nyama wenye meno makali na nyoka wenye sumu watambaao uvumbini. Upanga utawaua wana huko nje, namo nyumbani mwao yatakuwa mastusho; ndipo, watakapokufa vijana wa kiume na wa kike, hata wachanga pamoja na wazee. Ningesema: Na niwapeperushe, niwakomeshe watu, wasiwakumbuke tena. Lakini ninayaogopa matata ya adui, wale wapingani wao wasibishe kwamba: Mikono yetu ndiyo inayopasa kutukuzwa, kwani aliyeyafanya haya yote siye Bwana. Kwani ndio taifa la watu waliopotelewa na akili, kwa hiyo hakuna utambuzi unaooneka kwao. Kama wangekuwa werevu wa kweli, wangeijua maana yao haya, wangeutambua nao mwisho utakaowapata wenyewe. Inawezekanaje, mtu mmoja akifukuza watu elfu, au wawili wakikimbiza watu maelfu kumi? Sio kwa sababu yule aliye mwamba wao amekwisha kuwauza? Sio kwa sababu Bwana amewatia mikononi mwao wengine? Kwani mwamba wao wale si kama mwamba wetu, nao adui zetu wenyewe hawana budi kuviitikia. Kwani mizabibu yao ni ileile ya Sodomu, nayo mashamba yao ni yaleyale ya Gomora, maana zabibu zao ni zenye sumu, navyo vichala vyao ni vyenye uchungu. Kwa kuwa uchungu wa majoka nvinyo zao huwasha; kama sumu kali za pili zilivyo, ndivyo, zilivyo nazo. Kumbe haya hayakuwekwa na kufungiwa kwangu? Kumbe hayamo katika vilimbiko vyangu kwa kutiwa muhuri? Lipizi ni langu mimi, ni mimi nitakayelipisha. Miguu yao itakapoteleza, ndipo, litakapokuwa, kwani siku ya mwangamizo wao iko karibu, nayo yatakayowapata yanapiga mbio kufika upesi. Kwani Bwana atawaamulia walio ukoo wake, walio watumishi wake ndio, atakaowahurumia; atakapoziona nguvu za mikono yao kuwa zimekwisha kabisa, atakapoona, ya kama hakuna tena mwenye nguvu kwao wala kwao waliofungwa, wala kwao waliofunguliwa: ndipo, atakapouliza: Miungu yao iko wapi? Uko wapi mwamba wao, waliouegemea? Wako wapi walioyala mafuta ya ng'ombe zao za tambiko? Wako wapi waliozinywa mvinyo za vinywaji vyao vya tambiko? Na wainuke, wawasaidie ninyi wakija kwenu kuwakingia! Tazameni sasa: Mimi kama nilivyokuwa, ndivyo, nilivyo, hakuna Mungu tena kuliko mimi! Mimi ni mwenye kuua na mwenye kurudisha uzimani, ni mwenye kupiga kidonda, nami ni mwenye kuponya, hakuna awezaye kuokoa mkononi mwangu. Kwani nauinua mkono wangu kuuelekeza mbinguni kwamba: Hivyo nilivyo mwenye uzima kale na kale, nitakapounoa upanga wangu ulio wenye umeme, nao mkono wangu utakaposhika mapatilizo, ndipo, nitakapowalipiza wapingani wangu na kuwalipisha wachukivu wangu. Nitailewesha mishale yangu, izidi kunywa damu, nao upanga wangu utakula nyama, ni damu zao watakaouawa nazo zao watakaotekwa, ni nyama zao walio vichwa na watawalaji wa adui. Shangilieni, enyi wamizimu, pamoja nao walio ukoo wake! Kwani damu za watumishi wake huzilipizia kisasi, huwalipiza wapingani wake, awapatie upozi walio wenyeji wa nchi yake, walio ukoo wake. Mose akenda, akayasema maneno yote ya wimbo huu masikioni pa watu, yeye na Yosua, mwana wa Nuni. Mose alipokwisha kuwaambia Waisiraeli wote maneno haya yote, akawaambia: Yawekeni mioyoni mwenu maneno haya yote, mimi ninayowashuhudia leo, nanyi mwaagize wana wenu, wayaangalie na kuyafanya maneno yote ya Maonyo haya! Kwani hili si neno la kusimuliana tu ninyi kwa ninyi, ila ni uzima wenu. Nanyi mtakapolifanya neno hili, siku zenu zitakuwa nyingi za kukaa katika hiyo nchi, mnayoivukia Yordani, mwichukue, iwe yenu. Siku iyo hiyo Bwana akamwambia Mose kwamba: Kwenye milima hii ya Abarimu uupande huo mlima wa Nebo ulioko katika nchi ya Wamoabu, unaoelekea Yeriko, uitazame nchi ya Kanaani, mimi nitakayowapa wana wa Isiraeli, iwe yao. Utakapokwisha kuupanda mlima huo utakufa, uchukuliwe kwenda kwao walio ukoo wako, kama kaka yako Haroni alivyokufa mlimani kwa Hori na kuchukuliwa kwenda kwao walio ukoo wake. Kwani mlikataa kunitii katikati ya wana wa Isiraeli kwenye Maji ya Magomvi kule Kadesi katika nyika ya Sini, mkaacha kunitakasa katikati ya wana wa Isiraeli. Kwa sababu hii utaiona hiyo nchi mbele yako, lakini hutaingia katika hiyo nchi, nitakayowapa wana wa Isiraeli. Hii ndiyo mbaraka, Mose, yule mtu wa Mungu, aliyowabariki wana wa Isiraeli kabla ya kufa kwake, akasema: Bwana alitoka Sinai, akakuchelea kama jua toka Seiri, akautokeza mwanga wake toka mlimani kwa Parani, akaja na kutoka katikati yao maelfu kumi ya watakatifu, kuumeni kwake ukawaka moto uliowatokezea Maonyo. Kweli anayapenda makabila ya watu, watakatifu wake wote wamo mkononi mwako; nao walipokaa miguuni pako, kila mmoja akapokea neno lake lililompasa. Mose akatuagiza Maonyo, yawe fungu lao mkutano wa Yakobo, akawa mfalme kwake Yeshuruni, vichwa vyao hao watu walipokusanyika kwake pamoja nao wale walio mashina ya Isiraeli. Rubeni na awepo uzimani, asife, ijapo watu wake wahesabike. Nayo hii ni mbaraka ya Yuda, akasema: Bwana, uisikie sauti ya Yuda! Umwingize kwao walio ukoo wake! Kwani mikono yake itakapowapigia vita, nawe msaidie kuwashinda wapingani wake! Naye Lawi akamwambia: Mwanga wako na Kweli yako ni yao watu wako wamchao Mungu, uliowajaribu kule Masa na kuwagombeza kwenye Maji ya Magomvi. Ndio wanaowaambia baba zao na mama zao: Hatukuwaona, nao ndugu zao hawawatazami, wala wana wao hawawajui, kwani huliangalia Neno lako, hulishika Agano lako. Wao na wawafundishe Wayakobo maamuzi yako, nao Waisiraeli Maonyo yako, tena na wavukize mavukizo, yapate kuingia puani mwako, wakitoa ng'ombe nzima za tambiko pako pa kukutambikia. Bwana, zibariki nguvu zao nazo kazi za mikono yao, zikupendeze! Wapingani na wachukivu uwavunje viuno, wasiwainukie tena! Benyamini akamwambia: Mpendwa wa Bwana na akae kwake na kutulia! Bwana humfunika mchana kutwa na kukaa kati ya mabega yake. Naye Yosefu akamwambia: Nchi yako na iwe imebarikiwa naye Bwana, akiipatia kipaji kizuri cha mbinguni, ndio umande, nayo maji mengi yakaayo ndani ya nchi. Na aipatie nacho kipaji kizuri cha mazao, jua linayoyaivisha, nacho kipaji kizuri cha matunda ya kila mwezi! Na aipatie nayo yatokayo juu ya milima iliyo ya zamani, nacho kipaji kizuri cha vilima vilivyo vya kale na kale! Navyo vipaji vizuri vya nchi, navyo vijaavyo ndani yake! Upendeleo wake akaaye porini na ukijie kichwa chake Yosefu, juu ya utosi wake yeye aliyewekwa kwa kutengwa na ndugu zake! Mwanawe wa kwanza ni dume la ng'ombe lenye utukufu, kama pembe za nyati zilivyo, ndivyo, zilivyo nazo pembe zake; atakapozitumia atawakumba makabila ya watu, waanguke chini wote pia walioko huku hata mapeoni kwa nchi, kwani ndivyo, walivyo makumi ya maelfu ya Efuraimu, tena ndivyo, walivyo nayo maelfu ya Manase. Naye Zebuluni akamwambia: Zebuluni, zifurahie safari zako za baharini, nawe Isakari, yafurahie mahema yako! Wataalika makabila ya watu kuja mlimani; ndiko, watakakochinja ng'ombe za tambiko zilizo za kweli, kwani mafuriko ya bahari yatawanyonyesha, mpaka washibe, nazo zile mali nyingi zilizofichika mafukoni zitakuwa zao. Naye Gadi akamwambia: Atukuzwe aliyempatia Gadi nchi iliyo pana! Huota kama jike la simba, apate kurarua mikono na vichwa. Alipoiona nchi ya kwanza, ikawa yake, kwani huko aliwekewa kazi ya mwongozi. Lakini naye akaja kwao waliokuwa vichwa vya watu hawa, akaishindisha haki ya Bwana na kuyatimiza mashauri yake akiwa pamoja nao hao Waisiraeli. Naye Dani akamwambia: Dani ni mwana mchanga wa simba, hushambulia na kutoka Basani. Nafutali akamwambia: Nafutali atashiba yampendezayo, azidishiwe mbaraka ya Bwana; chukua nchi ya baharini na ya kusini, iwe yako! Naye Aseri akamwambia: Aseri ndiye katika hawa wana atakayepata mbaraka zaidi, tena atakuwa mpendwa wao ndugu zake, nao mguu wake atauchovya katika mafuta; makomeo yake yatakuwa ya chuma na ya shaba, nazo nguvu zako ziwe zizo hizo siku zote, utakazokuwapo. Mungu wake Yeshuruni, hakuna wa kufanana naye, ndiye anayepita juu mbinguni, akusaidie, namo mawinguni, auonyeshe utukufu wake. Yeye Mungu wa kale ni kimbilio, chini yako imekunjuliwa mikono iliyo ya kale na kale. Atawafukuza adui mbele yako akikuambia: Angamiza tu! Kwa hiyo Waisiraeli watakaa na kutulia vema, watakuwa pake yao kwenye chemchemi yake Yakobo katika nchi yenye ngano na mvinyo mbichi, nazo mbingu zake zitadondoa umande. Mwenye shangwe ni wewe, Isiraeli! Yuko nani aliyeokolewa na Bwana kama wewe? Yeye ni ngao inayokusaidia, tena ni upanga unaokupatia utukufu. Kwa hiyo adui zako watakunyenyekea, lakini wewe utatembea na kuvikanyaga vilima vyao. Kisha Mose akatoka kwenye mbuga za Moabu, akaupanda mlima wa Nebo ulio mrefu zaidi kuliko milima mingine ya Pisiga, unaoelekea Yeriko. Huko Bwana akamwonyesha nchi yote ya Gileadi mpaka nchi ya Dani, nayo nchi yote ya Nafutali, nayo nchi ya Efuraimu, nayo ya Manase, nayo nchi yote nzima ya Yuda mpaka kwenye bahari ya machweoni kwa jua, nayo nchi ya kusini, nayo nchi ya tambarare ya bondeni karibu ya Yeriko, ule mji wenye mitende, mpaka Soari. Kisha Bwana akamwambia: Hii ndiyo nchi, niliyomwapia Aburahamu na Isaka na Yakobo kwamba: Nchi hii nitawapa wao wa uzao wako. Basi, nimekuonyesha, uione kwa macho yako, lakini hutavuka kuiingia. Kisha Mose, mtumishi wa Bwana, akafa huko katika nchi ya Moabu, kwa kuwa Bwana aliviagiza hivyo. Akamzika huko katika bonde la nchi ya Moabu kulikoelekea Beti-Peori, lakini hakuna mtu anayelijua kaburi lake mpaka siku hii ya leo. Mose alikuwa mwenye miaka 120 alipokufa, macho yake yalikuwa hayakufifia, nazo nguvu zake za mwilini zilikuwa hazikupunguka. Wana wa Isiraeli wakamwombolezea Mose siku 30 katika mbuga za Moabu, hata siku za maombolezo ya matanga ya Mose zikatimia. Naye Yosua, mwana wa Nuni, alikuwa amejazwa roho ya werevu wa kweli, kwa kuwa Mose alimbandikia mikono yake. Kwa hiyo wana wa Isiraeli wakamsikia, wakafanya, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Kwao Waisiraeli hakuinuka tena mfumbuaji kama Mose, Bwana aliyejuana naye uso kwa uso, wala hakuna aliyefanana naye kwa kufanya vielekezo na vioja vyote, Bwana alivyomtuma katika nchi ya Misri kumfanyizia Farao nao watumishi wake wote na wenyeji wote wa nchi yake, wala hakuna aliyefanana naye kwa kufanya matendo yote ya nguvu za mikono yake wala kwa yale makuu yote ya kustusha, Mose aliyoyafanya machoni pao Waisiraeli wote. Mose, mtumishi wa Bwana, alipokwisha kufa, ndipo, Bwana alipomwambia Yosua, mwana wa Nuni, mtumishi wake Mose, kwamba: Mtumishi wangu Mose amekwisha kufa; sasa ondoka, uuvuke huu Yordani, wewe na watu wote wa ukoo huu, mwiingie nchi hiyo, mimi nitakayowapa wana wa Isiraeli. Kila mahali, nyayo za miguu yenu zitakapopakanyaga, nitawapa ninyi, kama nilivyomwambia Mose. Kutoka nyikani na huko Libanoni mpaka kwenye lile jito kubwa, lile jito la Furati, nchi yote nzima ya Wahiti, tena mpaka kwenye Bahari Kubwa iliyoko upande wa machweoni kwa jua; huko ndiko, mpaka wenu utakakokuwa. Siku zote, utakazokuwapo, hatakuwako mtu atakayesimama mbele yako. Kama nilivyokuwa na Mose, vivyo hivyo nitakuwa na wewe, sitakuepuka, wala sitakuacha. Jipe moyo, upate nguvu! Kwani wewe utawapeleka watu hawa, waichukue nchi hiyo, niliyowaapia baba zenu kuwapa. Ni hii tu: Jipe moyo, upate nguvu sana za kuyaangalia na kuyafanya Maonyo yote, mtumishi wangu Mose aliyokuagiza! Usiyaache kupitia kuumeni wala kushotoni, upate kujua njia ya kweli po pote, utakapokwenda. Kitabu cha Maonyo haya kisiondoke kinywani mwako, ila uyawaze moyoni mchana na usiku, upate kuyaangalia na kuyafanya yote yaliyoandikiwa humo, kwani ndivyo, utakavyofanikiwa katika njia zako kwa kuzijua zitakazokuwa za kweli. Sukukuagiza kujipa moyo, upate nguvu? Usiogope, wala usiingiwe na vituko! Kwani Bwana Mungu wako yuko pamoja na wewe po pote, utakapokwenda. Yosua akawaagiza wenye amri ya watu kwamba: Piteni makambini po pote, mwaagize watu kwamba: Jitengenezeeni pamba za njiani! Kwani baada ya siku tatu mtauvuka huu Yordani kwenda kuichukua hiyo nchi, Bwana Mungu wenu atakayowapa ninyi, mwichukue, iwe yenu. Nao Warubeni na Wagadi na nusu ya watu wa shina la Manese Yosua akaanza kuwaambia kwamba: Likumbukeni lile neno, Mose, mtumishi wa Bwana, alilowaagiza kwamba: Bwana Mungu enu atawapatia kutulia na kuwapa ninyi nchi hii. Wake na watoto na nyama wenu wa kufuga watakaa katika nchi hii, Mose aliyowapa ninyi ng'ambo hii ya Yordani; lakini ninyi nyote mlio mafundi wa vita wenye nguvu mtashika mata, mvuke na kuwatangulia ndugu zenu, mwasaidie. Tena hapo, Bwana atakapowapatia nao ndugu zenu kutulia kama ninyi, nao waichukue hiyo nchi, Bwana Mungu wenu watakavyowapa, iwe yao, ndipo, mtakaporudi katika nchi iliyo yenu wenyewe, mwichukue, iwe yenu kweli, ni hii, Mose, mtumishi wa Bwana, aliyowapa ninyi ng'ambo hii ya Yordani upande wa maawioni kwa jua. Wakamjibu Yosua kwamba: Yote, uliyotuagiza, tutayafanya, napo po pote, utakapotutuma, tutakwenda. Kama tulivyomsikia Mose katika mambo yote, hivyo tutakusikia hata wewe. Tunataka tu, Bwana Mungu wako awe na wewe, kama alivyokuwa na Mose. Kila mtu atakayekupingia, ukisema neno, asiyasikie maneno yako yote, utakayotuagiza, atauawa. Jipe moyo, upate nguvu! Yosua mwana wa Nuni, akatuma na kufichaficha toka Sitimu watu wawili kwenda kupeleleza, akiwaambia: Nendeni, mwitazame nchi hii nao mji wa Yeriko! Wakaenda, wakafikia nyumbani mwa mwanamke mgoni, jina lake Rahabu, wakalala huko. Mfalme wa Yeriko alipoambiwa: Tazama, wako watu waliotoka kwa wana wa Isiraeli, wamekuja usiku huu kuipeleleza nchi hii, mfalme wa Yeriko akatuma kwa Rahabu kumwambia: Watoe wale watu waliokuja kwako na kuingia nyumbani mwako, kwani wamekuja kuipeleleza nchi hii yote. Lakini yule mwanamke akawachukua wale watu wawili, akawaficha, kisha akasema: Kweli wale watu walifika kwangu, lakini sikujua, walikotoka. Tena hapo, malango yalipofungwa jioni, wale watu wakatoka, nami sikujua, wale watu walikokwenda. Wafuateni upesi kwa kupiga mbio, na mwakamate. Lakini alikuwa amewapandisha darini na kuwaficha katika makonge yaliyotandikwa naye huko darini. Nao wale watu wakawafuata upesi wakishika njia ya kwenda Yordani mpaka huko vivukoni. Hao waliowafuata upesi walipokwisha kutoka, wakalifunga lango la mji. Wale walipokuwa hawajalala bado, yule mwanamke akapanda darini na kufika huko, walikokuwa, akawaambia wale watu: Ninajua, ya kuwa Bwana amewapa nchi hii, asi tukaingiwa na mastuko kwa kuwaogopa ninyi, nao wenyeji wote wa nchi hii mioyo yao imeyeyuka kwa ajili yanu ninyi; kwani tumesikia, jinsi Bwana alivyokausha mbele yenu maji ya Bahari Nyekundu, mlipotoka Misri, tena mliyowatendea wale wafalme wawili wa Waamori, Sihoni na Ogi, waliokuwako ng'ambo ya huko ya Yordani, mliowaangamiza kabisa kwa kuwatia mwiko wa kuwapo. Tulipoyasikia, mioyo yetu ikayeyuka, hakuna mtu asiyekatika roho kwa ajili yenu, kwani Bwana Mungu wenu ni Mungu huko mbinguni juu, hata huku chini katika nchi. Sasa niapieni na kumtaja Bwana kwamba: Kama mimi nilivyowatendea mema, ndivyo, nanyi mtakavyoutendea mema mlango wa baba yangu, mnipe kielekezo cha welekevu wenu, mkiacha kuwaua akina baba na mama na ndugu zangu wa kiume na wa kike nao wote wa kwao, mkiziponya roho zetu, tusife. Wale watu wakawaambia: Tutazitoa roho zetu, ziwakomboe ninyi kufani, msipoyaeleza haya mambo yetu. Hapo, Bwana atakapotupa nchi hii, tutakufanyizia mambo mema yenye welekevu. Kisha akawashusha kwa kamba dirishani, kwani nyumba yake ilikuwa imejengwa juu ya boma la mji; hapo juu ya boma ndipo, alipokaa. Akawaambia: Nendeni milimani kujificha huko siku tatu, wanaowafuata wasiwapate! Wao wanaowafuata watakaporudi, basi, mtakwenda zenu. Wale watu wakamwambia: Kwa ajili ya hicho kiapo, ulichotuapisha, hatutakora manza, ila itakuwa hivyo: sisi tutakapoingia katika nchi hii, sharti ulifunge kamba hili la nyuzi nyekundu hapa dirishani, ulipotushusha, kisha baba yako na mama yako na ndugu zako nao wote walio wa mlango wa baba yako uwakusanye kwako humu nyumbani. Na viwe hivyo: kila atakayetoka milangoni: pa nyumbani mwako kwenda nje, damu yake itamjia kichwani pake, lakini sisi tutakuwa hatumo; lakini kila atakayekuwa kwako humu nyumbani, damu yake itatujia sisi vichwani petu, kama mkono wa mtu utampiga. Tena mtakapoyaeleza hayo mambo yetu, sisi tutakuwa hatufungwi tena na hicho kiapo, ulichotuapisha. Akawaambia: Kama mlivyosema, basi, na viwe hivyo. Kisha akawaondokesha, wakaenda zao, naye akalifunga lile kamba jekundu dirishani. Walipokwenda, wakaenda milimani, wakakaa huko siku tatu, mpaka wao waliowafuata wakirudi; nao hao waliowafuata waliwatafuta njiani po pote, lakini hawakuwaona. Kisha wale watu wawili wakarudi wakishuka milimani na kuvuka mtoni; walipofika kwake Yosua, mwana wa Nuni, wakamsimulia yote yaliyowapata. Wakamwambia Yosua: Kweli Bwana ameitia hiyo nchi yote mikononi mwetu, nao wenyeji wote wa nchi hiyo wameyeyuka mioyo kwa ajili yetu. Yosua akaamka asubuhi na mapema, wakaondoka kule Sitimu, wakaja Yordani, yeye na wana wote wa Isiraeli, wakalala huko kabla ya kuvuka. Siku tatu zilipopita, wenye amri wakazunguka makambini, wakawaagiza watu kwamba: Mtakapoliona Sanduku la Agano la Bwana Mungu wenu, watambikaji Walawi wakilichukua, nanyi mtaondoka mahali penu, mlifuate. Mtaangalia tu, hapo katikati yenu nalo hilo Sanduku pawe mahali penye urefu wa mikono elfu mbili, msilikaribie zaidi, mpate kuijua njia yenu ya kuishika, kwani hamtavuka katika njia ya siku zote. Kisha Yosua akawaambia watu: Jieueni! Kwani kesho Bwana atafanya vioja kwenu. Kisha Yosua akawaambia watambikaji kwamba: Lichukueni Sanduku la Agano, mwatangulie watu! Ndipo, walipolichukua Sanduku la Agano, wakawatangulia watu. Ndipo, Bwana alipomwambia Yosua: Siku hii ya leo nitaanza kukukuza machoni pa Waisiraeli wote, kwa kuwa watajua, ya kama nitakuwa na wewe, kama nilivyokuwa na Mose. Nawe uwaagize watambikaji wanaolichukua Sanduku la Agano kwamba: Mtakapofika ukingoni penye maji ya Yordani mtasimama. Yosua akawaambia wana wa Isiraeli: Fikeni karibu, myasikie maneno ya Bwana Mungu wenu! Kisha Yosua akawaambia: Hapo ndipo, mtakapojua, ya kuwa Mungu Mwenye usima yuko katikati yenu, atakapowafukuza kabisa mbele yenu Wakanaani na Wahiti na Wahiwi na Waperizi na Wagirgasi na Waamori na Wayebusi. Nanyi mtaliona sanduku la Agano la Bwana wa nchi zote, likiwatangulia kuuvuka Yordani. Kwa hiyo jichagulieni watu kumi na wawili katika mashina ya Waisiraeli, katika kila shina moja mtu mmoja! Itakuwa hapo, nyayo za miguu ya watambikaji wanaolichukua Sanduku la Agano la Bwana wa nchi zote zitakapoyagusa maji ya Yordani, ndipo, maji ya Yordai yatakapojitenga, hayo maji yanayoshuka nayo yanayotoka juu, haya yasimame kuwa kama boma moja tu. Watu walipoondoka mahemani kwao, wauvuke Yordani, watambikaji wakalichukua Sanduku la Agano kuwatangulia watu; basi, wachukuzi wa hilo Sanduku walipofika Yordani, nayo miguu yao watambikaji waliolichukua hilo Sanduku ilipojichovya ukingoni katika maji, kwani siku zote za mavuno Yordani hujaa maji mpaka juu ukingoni pande zote mbili, ndipo, maji yaliyotoka upande wa juu yaliposimama, yakafurika juu kuwa kama boma moja tu, yakafika mbali sana mpaka mji wa Adamu ulioko upande wa Sartani; nayo maji yaliyoshuka kuingia katika bahari ya nyikani, ile Bahari ya Chumvi, yakapwa yote pia; kwa hiyo watu wakapata kuvuka na kuuelekea mji wa Yeriko. Nao watambikaji waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana wakasimama katikati ya mto wa Yordani na kuishikiza miguu pakavu penyewe, nao Waisiraeli wote wakapitia pakavu; vikawa hivyo, hata watu wote wakaisha kuuvuka Yordani. Watu wote walipokwisha kuuvuka Yordani, Bwana akamwambia Yosua kwamba: Jichagulieni katika watu wa ukoo huu watu kumi na wawili, katika kila shina moja mtu mmoja! Kisha waagizeni kwamba: Chukueni katikati ya Yordani hapo, watambikaji waliposimama na kuishikiza miguu, mawe kumi na mawili, myapitishe mtoni kwenda nayo, myapeleke kambini, mtakakolala usiku huu. Ndipo, Yosua alipowaita wale watu kumi na wawili, aliowachagua katika wana wa Isiraeli, mtu mmoja katika kila shina moja, kisha Yosua akawaambia: Nendeni mbele penye Sanduku la Bwana Mungu wenu lililoko katikati ya Yordani, mjitwike kila mtu jiwe moja begani pake kwa hesabu ya mashina ya wana wa Isiraeli, hapo pawe kielekezo kwenu, kwani kesho wana wenu watawauliza kwamba: Haya mawe yenu maana yao nini? Ndipo, mtakapowaambia: Ni kwa kuwa maji ya Yordani yalikupwa mbele ya Sanduku la Agano la Bwana, lilipouvuka Yordani; hapo maji ya Yordani yalikupwa kabisa. Ndivyo, haya mawe yatakavyokuwa kikumbusho cha wana wa Isiraeli kale na kale. Wana wa Isiraeli wakafanya, kama Yosua alivyowaagiza, wakachukua mawe kumi na mawili hapo katikati ya Yordani, kama Bwana alivyomwambia Yosua, kwa hesabu ya mashina ya wana wa Isiraeli, wakayapitisha kwenda nayo kambini; ndiko walikoyaweka. Mawe kumi na mawili mengine Yosua akayasimika katikati ya Yordani hapo chini, watambikaji waliolichukua Sanduku la Agano walipoishikiza miguu yao, nayo yako huko mpaka siku hii ya leo. Lakini watambikaji waliolichukua hilo Sanduku walikuwa wanasimama katikati ya Yordani, mpaka mambo yote yakamalizika, Bwana aliyomwagiza Yosua kuwaambia watu, nayo yalikuwa sawa na yale, Mose aliyomwagiza Yosua. Nao watu wakavuka mbiombio. Ikawa, watu wote walipokwisha kuvuka, Sanduku la Bwana nalo likavuka pamoja na watambikaji machoni pa watu. Nao wana wa Rubeni na wana wa Gadi nao wa nusu ya shina la Manase wakavuka wenye mata yao na kuwatangulia wana wa Isiraeli, kama Mose alivyowaambia. Kikosi chao cha washika mata ya vita kilikuwa kama watu 40000 waliovuka machoni pa Bwana kwenda kupiga vita katika mbuga za Yeriko. Siku hiyo Bwana alimkuza Yosua machoni pa Waisiraeli wote, wakamwogopa, kama walivyomwogopa Mose siku zote, alizokuwapo. Kisha Bwana akamwambia Yosua kwamba: Waagize watambikaji wanaolichukua Sanduku la Ushahidi, wapande na kutoka Yordani. Ndipo, Yosua alipowaagiza watambikaji kwamba: Pandeni na kutoka Yordani! Ikawa, watambikaji waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana walipopanda na kutoka katikati ya Yordani, basi, nyayo za miguu ya hao watambikaji zilipoinuliwa kukanyaga pakavu, ndipo, maji ya Yordani yaliporudi mahali pao kuishika njia yao kama siku zote mpaka juu ukingoni pande zote mbili. Watu walipopanda kutoka Yordani, ilikuwa siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga makambi Gilgali kwenye mpaka wa Yeriko wa maaawioni kwa jua. Kisha yale mawe kumi na mawili, waliyoyachukua mle Yordani, Yosua akayasimika Gilgali, akawaambia wana wa Isiraeli kwamba: Watoto wenu watakapowauliza kesho baba zao kwamba: Haya mawe maana yao nini? mtawajulisha hiyo maana na kuwaambia: Waisiraeli waliuvuka huu mto wa Yordani pakavu, kwa kuwa Bwana Mungu wenu aliyapwesha maji ya Yordani mbele yenu, mpaka mwishe kuvuka, kama Bwana Mungu wenu alivyofanya penye Bahari Nyekundu, alipoipwesha mbele yetu, mpaka tuishe kuvuka. Ndipo, makabila yote ya nchi watakapoujua mkono wa Bwana kuwa wenye nguvu, kusudi mpate kumwogopa Bwana Mungu wenu siku zote. Wafalme wote wa Waamori waliokaa ng'ambo ya huku ya Yordani upande wa baharini nao wafalme wote wa Wakanaani waliokaa pwani waliposikia, jinsi Bwana alivyoyapwesha maji ya Yordani mbele ya wana wa Isiraeli, mpaka waishe kuvuka, mioyo yao ikayeyuka, hakuwako mtu wa kwao asiyezimia roho kwa ajili ya wana wa Isiraeli. Wakati huo Bwana akamwambia Yosua: Jitengenezee visu vya mawe makali, uwarudie wana wa Isiraeli kuwatahiri mara ya pili! Ndipo, Yosua alipojitengenezea visu vya mawe makali, akawatahiri wana wa Isiraeli katika Kilima cha Araloti (Tohara). Tena sababu yake Yosua ya kuwatahiri ilikuwa hii: watu wote waliotoka Misri waume wao wote walikuwa watu wa vita, nao walikufa nyikani njiani, walipokwisha kutoka Misri. Wale watu wote waliotoka walikuwa wametahiriwa, lakini wale watu wote waliozaliwa nyikani njiani, walipokwisha kutoka Misri, hawakutahiriwa. Kwani wana wa Isiraeli walizunguka nyikani miaka 40, mpaka wale watu wa vita wote pia waliotoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakuisikia sauti ya Bwana; kwa hiyo Bwana aliwaapia, wasiione ile nchi, yeye Bwana aliyowaapia baba zao, ya kama atatupa sisi, ni nchi hiyo inayochuruzika maziwa na asali. Kisha akawainua wana wao mahali pao; wao ndio, Yosua aliowatahiri, kwani walikuwa hawajatahiriwa bado, kwa kuwa njiani hawakuwatahiri. Nao hao wote walipokwisha kutahiriwa, wakakaa papo hapo makambini, mpaka waishe kupona. Kisha Bwana akamwambia Yosua: Zile soni, Wamisri walizowapatia, nimezifingirisha, ziwaondokee ninyi. Kwa hiyo walipaita mahali pale Gilgali (Mfingirisho) mpaka siku hii ya leo. Wana wa Isiraeli walipokaa makambini kule Gilgali wakala sikukuu ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi jioni kulekule katika nyika za Yeriko. Siku ya pili ya Pasaka wakala mazao ya nchi, mikate isiyochachwa na bisi; ndiyo, waliyoila siku hiyohiyo. Ndipo, Mana zilipokoma kesho yake hiyo siku, walipokula mazao ya nchi, wana wa Isiraeli wasizipate Mana tena; kwa sababu hii wakala mwaka huo mapato ya nchi ya Kanaani. Ikawa, Yosua alipokuwa huko karibu ya Yeriko, akayainua macho yake na kuchungulia, mara akaona mtu aliyesimama hapo na kumtazama, namo mkononi mwake alishika upanga uliokwisha kuchomolewa. Yosua alipomwendea na kumwuliza: Wewe u mtu wa kwetu au wa adui zetu? akasema: Sivyo, kwani mimi ni mkuu wa vikosi vya Bwana; nimefika sasa hivi. Ndipo, Yosua alipojiangusha chini kifudifudi, amwangukie, akamwuliza: Bwana wangu yuko na maneno gani ya kumwambia mtumishi wake? Naye mkuu wa vikosi vya Bwana akamwambia Yosua: Vivue viatu miguuni pako! Kwani mahali hapa, wewe unaposimama, ndipo patakatifu. Yosua akafanya hivyo. Wayeriko walikuwa wamefunga malango, nayo yakakaa hivyo, yalivyofungwa wa ajili ya wana wa Isiraeli, hakuwako aliyetoka wala aliyeingia. Bwana akamwambia Yosua: Tazama, huu mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake na mafundi wa vita walio wenye nguvu nimeutia mkononi mwako. Uzungukeni mji huu, ninyi wapiga vita wote, mwuzunguke wote pia mara moja! Fanyeni hivyo siku sita! Tena watambikaji saba na washike mabaragumu saba yenye milio mikubwa, walitangulie Sanduku la Agano! Siku ya saba sharti mwuzunguke mji huu mara saba, watambikaji wakiyapiga mabaragumu yao. Tena pembe ya kondo yenye mlio mrefu itakapopigwa, watu watakapozisikia sauti za mabaragumu, watu wote pia na wazomee mazomeo makubwa, ndipo, kuta za boma la mji zitakapoanguka chini, watu wenu wapate kupanda na kuingia mjini kila mtu hapo, anaposimama. Ndipo, Yosua, mwana wa Nuni, alipowaita watambikaji, akawaambia: Lichukueni Sanduku la Agano! Tena watambikaji saba na wachukue mabaragumu saba yenye milio mikubwa, walitangulie Sanduku la Bwana. Nao watu akawaambia: Nendeni kuuzunguka mji huu wote! Nao wenye mata na walitangulie Sanduku la Bwana! Yosua alipowaagiza watu hivyo, watambikaji saba wakachukua mabaragumu saba yenye milio mikubwa kwenda mbele ya Bwana, nao wakaenda wakiyapiga hayo mabaragumu, nalo Sanduku la Agano la Bwana likawafuata. Nao wenye mata walikwenda mbele ya watambikaji waliopiga mabaragumu, nao wafuasi wa nyuma walikwenda nyuma ya Sanduku hilo, wote walikuwa wanakwenda, mabaragumu yakilia. Lakini wale watu Yosua alikuwa amewaagiza kwamba: Msizomee! Wala sauti zenu zisisikilike! Wala neno lo lote lisitoke vinywani mwenu mpaka ile siku, nitakayowaambia: Zomeeni! Hapo ndipo, mtakapozomea. Basi, wakalizungusha Sanduku la Bwana na kuuzunguka mji huo wote mzima mara moja, kisha wakaingia makambini, wakalala humo makambini. Kesho yake Yosua akaamka na mapema, nao watambikaji wakalichukua Sanduki la Bwana. Nao wale watambikaji saba wakayachukua yale mabaragumu yenye milio mikubwa kwenda mbele ya Bwana; basi, walikuwa wanakwenda na kuyapiga hayo mabaragumu, nao wenye mata walikwenda mbele yao, nao wafuasi wa nyuma walikwenda nyuma ya Sanduku la Bwana; wote walikuwa wanakwenda, mabaragumu yakilia. Walipokwisha kuuzuguka huo mji mara moja siku ya pili, wakarudi makambini. Nidvyo, walivyofanya siku sita. Siku ya saba wakaamka asubuhi, mapambazuko yalipoanza, wakauzunguka huo mji mara saba vivyo hivyo, kama walivyofanya siku zote; lakini siku hiyo wakauzunguka huo mji mara saba. Ilipofika mara ya saba, watambikaji wale walipoyapiga mabaragumu, ndipo, Yosua alipowaambia watu: Zomeeni! Kwani Bwana amewapa mji huu. Lakini mji uwe wenye mwiko wa kuwapo, yote yaliyomo yawe mali za Bwana. Rahabu tu, yule mwanamke mgoni na apone pamoja nao wote waliomo nyumbani mwake, kwa kuwa aliwaficha wajumbe, niliowatuma. Jiangalieni sana kwa ajili yao yaliyo yenye mwiko, msiyatie kwanza mwiko, kisha mkachukua mengine yaliyo yenye mwiko. Kwani hivyo mtayapatia makambi ya Waisiraeli viapizo kwa kuyaponza Fedha zote na dhahabu na vyombo vya shaba na vya chuma ni mali za Bwana, sharti viingie katika kilimbiko cha Bwana. Ndipo, watu walipozomea, nayo mabaragumu yakapigwa; watu walipozisikia sauti za mabaragumu, nao wakazidi kuzomea mazomeo makubwa, ndipo, kuta za boma zilipoanguka chini, watu wakapanda kuuingia mji kila mtu hapo, aliposimama; ndivyo, walivyouteka huo mji. Wote waliokuwamo mjini wakawatia mwiko wa kuwapo, wakawaua kwa ukali wa panga, waume kwa wake, watoto kwa wazee, hata ng'ombe na kondoo na punda. Wale watu wawili walioipeleleza nchi hiyo Yosua akawaambia: Ingieni nyumbani mwake yule mwanamke mgoni, mmtoe mle nyumbani yule mwanamke nao wote waliomo mwake, kama mlivyomwapia. Ndipo, wale wapelelezi vijana walipoingia mwake, wakamtoa Rahabu na baba yake na mama yake na ndugu zake nao wote waliokuwa kwake, nao wote wa ukoo wake wakawatoa, wakawaweka mahali palipokuwa nje ya makambi ya Waisiraeli. Kisha huo mji wakauteketeza kwa moto pamoja navyo vyote vilivyokuwamo, lakini fedha na dhahabu na vyombo vya shaba na vya chuma wakavitia katika kilimbiko cha Nyumbani mwa Bwana. Lakini yule mwanamke mgoni Rahabu na mlango wa baba yake nao wote waliokuwa wake Yosua akawaacha, asiwaue, naye akakaa katikati ya Waisiraeli mpaka siku hii ya leo, kwa kuwa aliwaficha wajumbe, Yosua aliowatuma kupeleleza Yeriko. Kisha Yosua akawaapisha watu hao kwamba: Mtu na awe ameapizwa machoni pa Bwana atakayeinuka, aujenge tena mji huu wa Yeriko! Atakapoweka misingi yake, mwanawe we kwanza atakufa, tena atakapoyatia malango yake, mwanawe mdogo atakufa! Bwana akawa naye Yosua, nao uvumi wake ukasikilika katika nchi yote nzima. Wana wa Isiraeli wakakora manza kwa kuuvunja ule mwiko, kwani Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabudi, mwana wa Zera wa shina la Yuda, akachukua vitu vyenye mwiko; ndipo, makali ya Bwana yalipowawakia wana wa Isiraeli. Kisha Yosua akatuma watu kutoka Yeriko kwenda Ai ulioko karibu ya Beti-Aweni, upande wa maawioni kwa jua wa Beteli, akawaambia kwamba: Pandeni kuipeleleza nchi hiyo! Nao wale watu wakapanda kupeleleza Ai. Waliporudi kwa Yosua wakamwambia: Wasiende watu wote kupanda huko! Watu kama 2000 au 3000 watatosha, waupige Ai. Usiwasumbue watu wote pia! Kwani wao ni wachache. Kisha walipopanda kama watu 3000 kwenda huko, wakawakimbia watu wa Ai, nao watu wa Ai wakaua kwao kama 36, wakawakimbiza kuanzia kwenye lango la mji mpaka kufika Sebarimu, wakawaua huko penye mtelemko; ndipo, mioyo ya watu ilipoyeyuka kuwa kama maji. Naye Yosua akazirarua nguo zake, akajiangusha chini kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana mpaka jioni, yeye na wazee wa Waisiraeli, wakitia mavumbi vichwani pao. Kisha Yosua akaomba: Wewe Bwana Mungu, kwa nini umewavukisha watu hawa Yordani, ukitutia mikononi mwa Waamori, watuangamize? Ingetufaa sana kukaa ng'ambo ya huko ya Yordani! E Bwana! Nisemeje, kwa kuwa Waisiraeli wamewapa adui zao visogo? Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watakapovisikia, watatuzunguka, walitoweshe jina letu katika nchi hii. Nawe utafanya nini kwa ajili ya Jina lako kuu? Ndipo, Bwana alipomwambia Yosua; Inuka! Ni kwa sababu gani, ukianguka usoni pako? Waisiraeli wamekosa wasipolishika agano langu, nililowaagiza, kwa maana wamechukua vitu vyenye mwiko kwa kuviiba, wakavificha na kuvitia katika vyombo vyao. Kwa hiyo wana wa Isiraeli hawakuweza kusimama machoni pa adui zao, hawakuwa na budi kuwapa hao adui zao visogo, kwani wamejipatia kiapizo. Mimi sitaendelea kuwa nanyi, msipokitowesha hicho kiapizo katikati yenu. Inuka, uwaeue hawa watu na kuwaambia: Jieulieni siku ya kesho! Kwani hivyo ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Kiko kiapizo kilichoko katikati yenu, Waisiraeli; kwa hiyo hamtaweza kusimama machoni pa adui zenu, mpaka mkiondoe hicho kiapizo katikati yenu. Kesho asubuhi sharti mjilete hapa shina kwa shina, nalo shina, Bwana atakalolikamata, litajileta ukoo kwa ukoo, nao ukoo, Bwana atakaoukamata, utajileta mlango kwa mlango, nao mlango, Bwana atakaokamata, watu wake watajileta mmoja mmoja. Naye atakayekamatwa kuwa mwenye kiapizo atateketezwa kwa moto pamoja navyo vyote, alivyo navyo, kwa kuwa hakulishika agano la Bwana na kuwafanyizia Waisiraeli upumbavu. Kesho yake Yosua akaamka na mapema; naye alipowaleta Waisiraeli shina kwa shina, likakamatwa shina la Yuda. Alipozileta koo za Yuda, akaukamata ukoo wa Wazera; alipouleta ukoo wa Wazera mmoja mmoja, Zabudi akakamatwa. Alipouleta mlango wake mmoja mmoja, akakamatwa Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabudi, mwana wa Zera wa shina la Yuda. Ndipo, Yosua alipomwambia Akani: Manangu, mche Bwana Mungu wa Isiraeli na kumtukuza, ukimwungamia waziwazi! Nielezee uliyoyafanya, usiyafiche! Akani akamjibu Yosua na kumwambia: Kweli, mimi nimemkosea Bwana Mungu wa Isiraeli nikifanya hivi na hivi. Nilipoona katika nyara vazi zuri la Babeli na fedha 200 na ulimi mmoja wa dhahabu wenye uzito wa sekeli 50, ndio ratli mbili, nikaingiwa na tamaa navyo, nikavichukua, viko hemani mwangu, vimefukiwa mchangani, nazo fedha ziko chini yao. Yosua akatuma wajumbe, wakapiga mbio kwenda hemani, wakaviona, vimefichwa hemani mwake, nazo fedha zilikuwa chini yao. Wakavichukua mle hemani, wakavipeleka kwa Yosua, wana wote wa Isiraeli walikokuwa, wakaviweka huko mbele yake Bwana. Kisha Yosua akamchukua Akani, mwana ma Zera, pamoja na zile fedha na lile vazi na ule ulimi wa dhahabu, hata wanawe wa kiume na wa kike, na ng'ombe wake na punda wake na mbuzi na kondoo wake na hema lake navyo vyote vilivyokuwa vyake, nao Waisiraeli wote wakaenda naye, wakawapeleka wote katikati ya bonde la Akori. Huko Yosua akasema: Kama ulivyotupatia mabaya, ndivyo Bwana akupatie mabaya nawe siku hii ya leo! Ndipo, Waisiraeli wote walipompiga mawe, navyo vile vitu wakavichoma moto, nao wale watu wakawaua kwa kuwapiga mawe. Kisha wakakusanya juu yake chungu kubwa la mawe lililoko mpaka siku hii ya leo. Ndipo, Bwana alipoyaacha makali yake yenye moto. Kwa hiyo wakaliita jina lake mahali pale Bonde la Akori (Bonde la Mabaya) mpaka siku hii ya leo. Kisha Bwana akamwambia Yosua: Usiogope, wala usiingiwe na vituko! Wachukue watu wote kwenda vitani pamoja na wewe! Kisha ondoka kuupandia Ai! Tazama, nimemtia mfalme wa Ai mkononi mwako pamoja na watu wake na mji wake na nchi yake. Nawe uufanyizie Ai na mfalme wake, kama ulivyoufanyizia Yeriko na mfalme wake, vitu vyake tu mtakavyoviteka pamoja na nyama wao wa kufuga mtajichukulia, viwe mateka yenu. Jipatie penye kuuvizia mji upande wake wa nyuma! Ndipo, Yosua alipoondoka pamoja na watu wote kwenda vitani kwa kuupandia Ai. Yosua akachagua watu 30000 walio mafundi wa vita wenye nguvu, akawatuma kwenda usiku alipokwisha kuwaagiza kwamba: Tazameni, ndivyo mwuvizie huu mji upande wa nyuma ya mji! msiupite mji kwenda mbali sana, nyote mpata kuwa tayari! Nami pamoja na watu wote walio kwangu tutaukaribia mji. Tena watakapotoka, watujie kama ile mara ya kwanza, tutakimbia mbele yao. Ndipo, watakapotoka, watufuate, mpaka tuishe kuwafungia njia ya kurudia mjini, kwani watasema: Wanatukimbia kama mara ya kwanza; nasi tunataka kweli kuwakimbia. Ndipo, ninyi mtakapoondoka hapo pa kuvizia, mwuteke mji, kwani Bwana Mungu wenu amaeutia mikononi mwenu. Hapo mtakapouteka mji, mwuteketeze kwa moto, mfanye, kama Bwana alivyosema! Yaangalieni, niliyowaagiza! Kisha Yosua akawatuma, nao wakaenda mahali pa kuvizia, wakakaa katikati ya Beteli na ya Ai upande wa baharini wa Ai. Naye Yosua akalala usiku huo katikati ya watu. Kesho yake Yosua akaamka na mapema, akawakagua watu wake, kisha akapanda yeye pamoja wa wazee wa Waisiraeli na kuwaongoza watu kwenda Ai. Nao wapiga vita wote waliokuwa naye wakapanda kuukaribia mji; walipofika ng'ambo ya huku ya mji wakalala upande wa kaskazini wa Ai, napo hapo katikati yao na mji wa Ai palikuwa bonde. Akachukua kama watu 5000, akawaweka pa kuvizia katikati ya Beteli na Ai upande wa baharini wa mji. Kisha wakayapanga majeshi yote ya watu waliokuwako upande wa kaskazini wa mji nao wale washambuliaji waliokuwako upande wa baharini wa mji. Kisha Yosua akaenda usiku huo kuja katikati ya bondeni. Mfalme wa Ai alipoviona, watu wa mji wakajidamka kwa upesi kuwaendea Waisiraeli kupigana nao, yeye na watu wake wote, mahali palepale mbele ya mbuga. Naye hakujua, ya kuwa wako wanaomvizia nyuma ya mji. Ndipo, Yosua na Waisiraeli wote walipojifanya kuwa kama watu waliopigwa nao, wakakimbia na kushika njia ya kwenda nyikani. Nao watu wale waliokuwamo mjini wakaitana kwenda kuwakimbiza, nao walipomkimbiza Yosua wakajitenga na mji wa kwao. Hakusalia mtu mle Ai wala Beteli asiyetoka kuwakimbiza Waisiraeli, nao mji wao wakauacha wazi wakiwakimbiza Waisiraeli. Ndipo, Bwana alipomwambia Yosua: Mkuki uliomo mkononi mwako, uunyoshee mji wa Ai! Kwani nitautia mkononi mwako. Yosua akaunyosha mkuki uliokuwamo mkononi mwake na kuuelekezea huo mji. Alipounyosha mkono wake, ndipo, wale waliouvizia walipoondoka upesi mahali pao na kupiga mbio, wakaingia katika mji, wakauteka, wakajihimiza kuuteketeza kwa moto. Watu wa Ai walipogeuka nyuma yao kutazama, mara wakaona, moshi wa mjini unavyopanda mbinguni juu, nao kwa kulegea mikono hawakuweza kukimbia, wala huko, wala huko; ndipo, wale watu waliokimbia nyikani walipowageukia wao waliowakimbiza. Yosua na Waisiraeli wote walipoona, ya kuwa waviziaji wameuteka mji, kwa kuwa moshi wa mjini ulipanda juu, nao wakarudi, wakawapiga watu wa Ai. Nao wale wa mjini wakatoka kuwaendea nao; ndivyo, hao walivyokuwa katikati ya Waisiraeli, hawa huku nao wale huko, wakawapiga, wasisaze hata mmoja aliyekimbia na kujiponya. Lakini mfalme wa Ai wakamkamata, yu hai, wakampeleka kwake Yosua. Nao Waisiraeli walipokwisha kuwaua mashambani na nyikani wenyeji wote wa Ai waliowakimbiza, basi, hao wote walipokwisha kuuawa kwa ukali wa panga, mpaka waishe kabisa, Waisiraeli wote wakarudi Ai, wakawaua wote waliokuwamo kwa ukali wa panga. Nao wote waliouawa siku hiyo, waume kwa wake, walikuwa 12000, ndio watu wote wa Ai. Kwani Yosua hakuurudisha mkono wake ulioshika mkuki, mpaka akiwaangamiza kabisa wenyeji wa Ai wote pia. Ni nyama wa kufuga tu na vitu, Waisiraeli walivyoviteka humo mjini, wakajichukulia kwa lile neno la Bwana, alilomwagiza Yosua. Kisha Yosua akauteketeza mji wa Ai, akaugeuza kuwa chungu tupu kale na kale mpaka siku hii ya leo. Naye mfalme wa Ai akamtungika mtini na kumwacha huko mpaka jioni; lakini jua lilipokuchwa, Yosua akaagiza, waushushe mzoga wake mtini, wautupe pa kuliingilia lango la mji, kisha wakakusanya juu yake chungu kubwa la mawe lililoko hata siku hii ya leo. Kisha Yosua akajenga juu ya mlima wa Ebali pa kumtambikia Bwana. Kama Mose, mtumishi wa Bwana, alivyowaagiza wana wa Isiraeli, kama vilivyoandikwa katika kitabu cha Maonyo ya Mose, alipajenga pale pa kutambikia kwa mawe mazima yasiyochongwa kwa chuma cha mtu, akamtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, wakachinja hata ng'ombe za tambiko za shukrani. Kisha akaandika hapo penye yale mawe mwandiko wa pili wa Maonyo ya Mose, aliouandika machoni pa wana wa Isiraeli. Nao Waisiraeli wote, wazee wao na wenye amri na waamuzi wao walikuwa wamesimama huku na huko penye lile Sanduku na kuwaelekea watambikaji Walawi waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana, wageni pamoja na wazalia, nusu yao waliuelekea mlima wa Gerizimu, nusu waliuelekea mlima wa Ebali, kama Mose, mtumishi wa Bwana, alivyowaagiza kale kuubariki ukoo wa Waisiraeli. Baadaye akayasoma maneno yote ya Maonyo, ya mbaraka nayo ya kiapizo, sawasawa kama yalivyoandikwa katika kitabu cha Maonyo. Katika yale yote, Mose aliyoyaagiza, halikuwamo hata moja, Yosua asilolisoma masikioni pa mkutano wa Waisiraeli wote, wakiwa pamoja na wanawake na wana wa wageni waliokwenda kukaa nao. Walipoyasikia hayo wafalme wote waliokaa ng'ambo ya huku ya Yordani milimani na katika nchi ya tambarare na huko pwani po pote penye Bahari Kubwa panapoelekea Libanoni. Wahiti na Waamori na Wakanaani na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi, wakakusanyika pamoja kwenda kupigana na Yosua nao Waisiraeli, mioyo yao ikawa kama mmoja. Wenyeji wa Gibeoni walipoyasikia, Yosua aliyoutendea Yeriko na Ai, wao wakatumia ujanja, wakajifanya kuwa wajumbe, wakawatandika punda wao magunia machakavu, wakachukua viriba vichakavu vya mvinyo vilivyotiwa viraka kwa kupasukapasuka. Miguuni wakavaa viatu vichakavu vilivyoshonwashonwa, miilini wakavaa nguo chakavu, nayo mikate yote ya pamba zao za njiani ilikuwa mikavu yenye ukungu. Kisha wakaenda Gilgali makambini kwake Yosua, wakamwambia yeye, nao Waisiraeli: Tumetoka nchi ya mbali, sasa fanyeni maagano nasi! Waisiraeli walipowaambia hao Wahiwi: Labda ninyi mnakaa katikati yetu, kwa hiyo tutawezaje kufanya maagano nanyi? wao wakamwambia Yosua: Sisi tu watumwa wako, naye Yosua akawauliza: Ninyi m wa nani? Tena mmetoka wapi? Wakamwambia: Watumwa wako wametoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya Jina la Bwana Mungu wako, kwani tumeusikia uvumi wake nayo yote, aliyoyafanya huko Misri, nayo yote, aliyowafanyia wale wafalme wawili wa Waamori waliokuwako ng'ambo ya huko ya Yordani, yule Sihoni, mfalme wa Hesiboni, na Ogi, mfalme wa Basani, aliyekaa Astaroti. Kwa hiyo wazee wetu na wenyeji wote wa nchi yetu wakatuambia kwamba: Chukueni mikononi mwenu pamba za njiani, mwende kukutana nao, mwaambie: Sisi tu watumwa wenu, sasa fanyeni maagano nasi! Hii mikate yetu ilikuwa yenye moto, tulipoichukua nyumbani mwetu kuwa pamba zetu siku hiyo, tulipotoka kwetu kwenda kwenu; sasa itazame, ni mikavu yenye ukungu! Hivi viriba vya mvinyo navyo vilikuwa vipya, tulipovijaza, sasa vitazame, vimepasukapasuka. Hizi nguo zetu nazo zimechakaa pamoja na viatu, kwa kuwa njia ni ya mbali sana. Ndipo, wale watu wa Kiisiraeli walipoonja pamba zao, lakini kinywa cha Bwana hawakukiuliza. Kisha Yosua akapatana nao kufanya maagano, asiwaue, nao wakuu wa mkutano wakawaapia hivyo. Siku tatu zilipopita walipokwisha kufanya hayo maagano nao, wakasikia, ya kuwa wale wanakaa karibu katika nchi iyo hiyo, waliyoikaa wenyewe. Ndipo, wana wa Isiraeli walipoondoka, wakaingia siku ya tatu mjini kwao, nayo miji yao ilikuwa Gibeoni na Kefira na Beroti na Kiriati-Yearimu. Lakini wana wa Isiraeli hawakuwaua, kwa kuwa wakuu wa mkutano waliwaapia na kumtaja Bwana Mungu wa Isiraeli. Wao wa mkutano wote walipowanung'unikia wakuu, wakuu wote wakauambia mkutano wote: Sisi tumewaapia na kumtaja Bwana Mungu wa Isiraeli, kwa hiyo sasa hatuwezi kuwagusa. Lakini nao tuwafanyie hivyo: tuache kuwaua, makali yasitujie kwa ajili ya hicho kiapo, tulichowaapia. Kwa hiyo wakuu wakawaambia: Na wakae uzimani! Lakini watakuwa wachanja kuni na wachota maji yao wote wa mkutano huu, kama wakuu walivyowaambia. Kisha Yosua akawaita, akawaambia kwamba: Mbona mmetudanganya na kutuambia: Sisi tunawakalia mbali sana? Nanyi mnakaa huku kwetu katikati! Sasa mtakuwa mmeapizwa, kwenu wasikoseke watumwa wa kuchanja kuni na wa kuchota maji yao walio mlango wa Mungu wangu! Nao wakamjibu Yosua wakisema: Watumwa wako walipashwa habari za kwamba: Bwana Mungu wako alimwagiza mtumishi wake Mose kuwapa ninyi nchi hii yote nzima, mwangamize wenyeji wote wa nchi hii, watoweke mbele yenu. Kwa hiyo tukaingiwa na oga mwingi rohoni mwetu wa kuwaogopa ninyi, kwa hiyo tukalifanya jambo lile. Sasa tazama, tumo mkononi mwako! Utakapoyaona kuwa mema yanyokayo, basi, tufanyizie kabisa! Kisha akawafanyizia hayo, akawaponya mikononi mwao wana wa Isiraeli, wasiwaue. Ndivyo, Yosua alivyowaweka siku hiyo kuwa wachanja kuni na wachota maji wa mkutano na wa mahali hapo pa kutambikia, Bwana atakapopachagua; vikawa hivyo mpaka siku hii ya leo. Ikawa, Adoni-Sedeki, mfalme wa Yerusalemu, aliposikia, ya kuwa Yosua ameuteka Ai na kuutia mwiko wa kuwapo, ya kuwa Waai na mfalme wao amewafanyizia yaleyale, aliyoufanyizia Yeriko na mfalme wake, tena ya kuwa wenyeji wa Gibeoni wamepatana nao Waisiraeli, wakapata kukaa katikati yao: wakaingiwa na woga kabisa, kwani Gibeoni ulikuwa mji mkubwa kama mji mwingine wo wote katika ufalme wake, tena ni mkubwa kuliko Ai, nao watu wake wote walikuwa mafundi wa vita. Kwa hiyo Adoni-Sedeki, mfalme wa Yerusalemu, akatuma kwa Hohamu, mfalme wa Heburoni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarmuti, na kwa Yafia, mfalme wa Lakisi, na kwa Debiri, mfalme wa Egloni, kwamba: Pandeni kuja kwangu, mnisaidie, tuwapige Wagibeoni, kwa kuwa wamepatana naye Yosua nao wana wa Isiraeli! Ndipo, walipokusanyika kwenda vitani hawa wafalme watano wa Waamori, mfalme wa Yerusalemu na mfalme wa Heburoni na mfalme wa Yarmuti na mfalme wa Lakisi na mfalme wa Egloni, wao na majeshi yao, wakapiga makambi huko Gibeoni kuupelekea vita. Ndipo, watu wa Gibeoni walipotuma Gilgali makambini kwa Yosua kwamba: Usiilegeze mikono yako ukiacha kuwasaidia watumwa wako! Ila panda upesi kuja kwetu, utuokoe na kutusaidia! Kwani wafalme wote wa Waamori wanaokaa milimani wametukusanyikia. Ndipo, Yosua alipotoka Gilgali kupanda kwao, yeye nao wapiga vita wote waliokuwa naye, nao hao wote walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu. Naye Bwana akamwambia Yosua: Usiwaogope! Kwani nimewatia mikononi mwako, hakuna mtu wa kwao atakayesimama usoni pako. Ndipo, Yosua alipowaendea akitoka Gilgali kwenda usiku kucha, awashambulie kwa mara moja. Naye Bwana akawastusha, walipowaona Waisiraeli, wakawapiga kule Gibeoni pigo kubwa wakiwafukuza, waikimbilie njia ya kupandia Beti-Horoni, wakawapiga hata kufika Azeka na Makeda. Ikawa, walipowakimbia Waisiraeli, walipofika pa kushukia Beti-Horoni, Bwana akawanyeshea mvua ya mawe makubwa toka mbinguni, mpaka wafike Azeka na kuuawa vivyo hivyo; nao waliouawa na mvua ya mawe walikuwa wengi kuliko wao, wana wa Isiraeli waliowaua kwa panga. Siku hiyo, Bwana alipowatoa Waamori machoni pa wana wa Isiraeli, ndipo, Yosua alipomwomba Bwana akisema masikioni pa Waisiraeli: Jua, simama kimya huko Gibeoni! Nawe mwezi, bondeni kwa Ayaloni! Ndipo, jua liliposimama kimya, nao mwezi ukasimama, hata watu wawalipize adui zao. Kumbe haya hayakuandikwa katika kitabu cha Mnyofu? Basi, jua likasimama katikati ya mbinguni, lisijihimize kuchwa muda kama wa siku nzima. Siku ndefu kama hiyo haikuwa mbele yake wala nyuma yake, Bwana alipoisikia sauti ya mtu wake, kwani ndivyo, Bwana alivyowagombea Waisiraeli. Kisha Yosua akarudi makambini kwa Gilgali pamoja na Waisiraeli wote waliokuwa naye. Wale wafalme watano wakakimbia, wakajificha pangoni kule Makeda. Yosua alipopashwa habari kwamba: Hao wafalme watano wameonekana, wamejificha pangoni huko Makeda, Yosua akaagiza: Poromosheni mawe makubwa hapo pa kuliingilia lile pango, kisha wekeni hapo watu wa kuwaangalia! Lakini ninyi msisimame bure! Ila pigeni mbio kuwafuata adui zenu, mwaue walio nyuma yao, msiwaache, waingie mjini kwao! Kwani Bwana Mungu wenu amewatia mikononi mwetu. Ikawa, Yosua na wana wa Isiraeli walipokwisha kuwapiga pigo hili kubwa sana, hata wamalizike, nao waliopona kwa kukimbia walipokwisha kuingia miji yenye maboma, ndipo, watu wote waliporudi salama makambini kwa Yosua kule Makeda, hakuna mtu tena aliyeuchongoa ulimi wake kuwasimanga wana wa Isiraeli. Kisha Yosua akaagiza: Pafungueni pa kuliingilia lile pango, mwatoe wale wafalme watano mle pangoni na kuwaleta kwangu! Wakafanya hivyo, wakawatoa wale wafalme watano pangoni, wakawapeleka kwake; ni mfalme wa Yerusalemu na mfalme wa Heburoni na mfalme wa Yarmuti na mfalme wa Lakisi na mfalme wa Egloni. Ikawa, walipowatoa hawa wafalme na kuwapeleka kwa Yosua, Yosua akawaita Waisiraeli wote, akawaambia wakuu wa wapiga vita waliokwenda naye: Karibuni, mwiweke miguu yenu juu ya kosi za wafalme hawa! Ndipo, walipowakaribia, wakaiweka miguu yao juu ya kosi zao. Yosua akawaambia: Msiogope, wala msiingiwe na vituko! Jipeni mioyo, mpate nguvu! Kwani hivyo ndivyo, Bwana atakavyowafanyizia adui zenu wote, mtakapopigana nao. Baadaye Yosua akawapiga na kuwaua, kisha akawatungika katika miti mitano; nao wakawa wakining'inia mpaka jioni. Ikawa hapo, jua lilipokuchwa, Yosua akatoa amri, ndipo, walipowashusha katika hiyo miti, wakawatupa mle pangoni, walimokuwa walijificha, wakaweka mawe makubwa hapo pa kuliingilia lile pango, nayo yako palepale hata siku hii ya leo. Siku hiyo Yosua akauteka Makeda; waliokuwamo akawaua kwa ukali wa panga, hata mfalme wake, akiwatia mwiko wa kuwapo wao wote pia waliokuwamo, wasiachwe kabisa, hakusaza hata mmoja aliyekimbia; naye mfalme wa Makeda akamfanyizia yaleyale, aliyomfanyizia mfalme wa Yeriko. Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye walipoondoka Makeda, wakaenda Libuna, wakapiga vita nao Walibuna. Bwana akautia nao mji huu pamoja na mfalme wake mikononi mwa Waisiraeli, wakawapiga kwa ukali wa panga wote pia waliokuwamo, hawakusaza hata mmoja aliyekimbia; naye mfalme wake wakamfanyizia yaleyale, waliyomfanyizia mfalme wa Yeriko. Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye walipoondoka Libuna wakaenda Lakisi, wakapiga makambi huko, wapigane nao. Bwana akautia Lakisi mikononi mwa Waisiraeli, wakauteka siku ya pili, wakawapiga kwa ukali wa panga wote pia waliokuwamo, wakawafanyizia yote, waliyowafanyizia Walibuna. Siku hizo ndipo, Horamu, mfalme wa Gezeri, alipopanda kuusaidia mji wa Lakisi, lakini Yosua akampiga pamoja na watu wake, asisaze kwake hata mmoja aliyekimbia. Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye walipoodoka Lakisi wakaenda Egloni, wakapiga makambi huko, wapigane nao. Wakauteka siku hiyo, wakawapiga kwa ukali wa panga wakiwatia mwiko wa kuwapo wao wote pia waliokuwamo, wasiachwe kabisa siku hiyo, wakawafanyizia yote, waliyowafanyizia Walakisi. Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye walipoondoka Egloni wakaenda Heburoni, wakapiga vita nao. Walipouteka wakawapiga watu kwa ukali wa panga pamoja na mfalme wa huko, hata miji yake yote; kwao wote waliokuwamo hawakusaza hata mmoja aliyekimbia, wakiyafanya yote, waliyowafanyizia Waegloni na kuwatia mwiko wa kuwapo wao wote waliokuwamo, wasiachwe kabisa. Kisha Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye wakaurudia Debira, wakapiga vita nao. Akamkamata mfalme na kuiteka miji yake yote, nao watu wakawapiga kwa ukali wa panga, wakiwatia mwiko wa kuwapo wao wote pia waliokuwamo, wasiachwe kabisa, hawakusaza hata mmoja aliyekimbia; kama walivyowafanyizia Waheburoni, ndivyo, walivyowafanyizia Wadebira nao; naye mfalme wa huko wakamfanyizia yaleyale, waliyowafanyizia Walibuna na mfalme wao. Ndivyo, Yosua alivyoipiga hiyo nchi yote, ile ya milimani nayo ya kusini nayo ya nchi ya tambarare nayo ya matelemko pamoja na wafalme wao, hakusaza hata mmoja aliyekimbia. Wenye kuvuta pumzi wote akawatia mwiko wa kuwapo, wasiachwe kabisa, kama Bwana Mungu wa Isiraeli alivyoagiza. Yosua akawapiga kutoka Kadesi-Barnea mpaka Gaza, nayo nchi yote ya Goseni mpaka Gibeoni. Wafalme hao wote Yosua akawateka pamoja na nchi zao kwa mara moja, kwani Bwana Mungu wa Isiraeli aliwapigia Waisiraeli vita. Kisha Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye wakarudi Gilgali makambini. Ikawa, Yabini, mfalme wa Hasori, alipoyasikia, akatuma kwa Yobabu, mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Simuroni na kwa mfalme wa Akisafu, na kwa wafalme waliokuwako kaskazini milimani na nyikani upande wa kusini wa Kineroti (Genezareti) na katika nchi ya tambarare na vilimani kwa Dori huko baharini, hata kwa Wakanaani waliokaa upande wa maawioni kwa jua na upande wa baharini na kwa Waamori na kwa Wahiti na kwa Waperizi na kwa Wayebusi milimani na kwa Wahiwi waliokaa chini kwa Hermoni katika nchi ya Misipa. Wakatoka wao pamoja na majeshi yao, wakawa watu wengi, kama mchanga ulioko ufukoni kwenye bahari ulivyo mwingi; walikuwa hata na farasi na magari mengi sana. Hawa wafalme wote walipokwisha kupatana mashauri, wakaenda, wakapiga makambi pamoja kwenye ziwa la Meromu, wapate kupigana nao Waisiraeli. Lakini Bwana akamwambia Yosua: Usiwaogope! Kwani kesho saa zizi hizi mimi nitawatoa wao wote, kuwa wamekwisha kuuawa na Waisiraeli, nao farasi wao na uwakate mishipa, nayo magari yao na uyachome moto. Ndipo, Yosua na wapiga vita wote waliokuwa naye walipowaendea huko kwenye ziwa la Meromu, mara wakawashambulia, naye Bwana akawatia mikononi mwa Waisiraeli, wakawapiga, wakawakimbiza mpaka Sidoni ulio mkuu na mpaka Misirefoti-Maimu (Maji Kupwa) na mpaka bondeni kwa Misipe upande wa maawioni kwa jua, wakawapiga, wasisaze hata mmoja aliyekimbia. Yosua akawafanyizia, kama Bwana alivyomwagiza, farasi wao akawakata mishipa, nayo magari yao akayachoma moto. Wakati huo Yosua akarudi, akauteka Hasori, naye mfalme wake akamwua kwa upanga, kwani kale Hasori ulikuwa mji mkuu wa hizi nchi za kifalme zote. Wakawapiga wote pia waliokuwamo kwa ukali wa panga wakiwatia wote waliovuta pumzi mwiko wa kuwapo, hakusalia hata mmoja; nao mji wa Hasori akauteketeza kwa moto. Nayo miji yote ya hao wafalme Yosua akaiteka pamoja na wafalme wao, akawapiga kwa ukali wa panga akiwatia mwiko wa kuwapo, wasiachwe kabisa, kama Mose, mtumishi wa Bwana, alivyowaagiza. Lakini miji yote iliyokuwa juu ya vilima vyao Waisiraeli hawakuiteketeza, Hasori peke yake tu Yosua aliuteketeza. Nazo nyara zote za humo mijini pamoja na nyama wa kufuga wana wa Isiraeli wakawachukua, lakini watu waliwaua wote kwa ukali wa panga, mpaka wawaangamize kabisa, hawakusaza ye yote aliyevuta pumzi. Kama Bwana alivyomwagiza mtumishi wake Mose, ndivyo, Mose naye alivyomwagiza Yosua, navyo ndivyo, Yosua alivyovifaanya: yale maneno yote, Bwana aliyomwagiza Mose, hakutengua hata moja, asilifanye. Ndivyo, Yosua alivyoiteka hiyo nchi nzima, ile ya milimani nayo ya upande wa kusini nayo nchi yote ya Goseni nayo nchi ya tambarare nayo ya nyika nayo milima ya Isiraeli pamoja na nchi yao ya tambarare, toka ile milima mitupu inayoendelea hata Seiri, mpaka Baali-Gadi katika bonde la Libanoni chini ya mlima wa Hermoni; nao wafalme wao wote Yosua akawateka, akawapiga na kuwaua. Siku nyingi Yosua alipiga vita nao hao wafalme wote. Haukuwako mji uliofanya mapatano na wana wa Isiraeli, wasipokuwa wale Wahiwi waliokaa Gibeoni; yote mingine waliichukua kwa kupiga vita. Kwani hili nalo lilitoka kwa Bwana, akiishupaza mioyo yao, waende kupiga vita na Waisiraeli, ule mwiko wa kuwapo waliotiwa umalizike, wasijipatie upendeleo, ila mwangamizo wao tu, kama Bwana alivyomwagiza Mose. Wakati huo Yosua akaenda kuwang'oa Waanaki milimani kwa Heburoni na kwa Debiri na kwa Anabu na milimani ko ote kwa Wayuda na milimani ko kote kwa Waisiraeli, Yosua akawatia mwiko wa kuwapo wao wenyewe na miji yao, wasiachwe kabisa. Hawakusalia Waanaki katika nchi ya wana wa Isiraeli, ni kule Gaza tu na Gadi na Asdodi; ndiko, walikosalia. Yosua akaichukua hiyo nchi yote nzima, kama Bwana alivyomwambia Mose, kisha Yosua akaigawia Waisiraeli, iwe fungu lao, kama walivyogawanyika kwa mashina yao. Kisha nchi ikapata kutulia, kwani vita vilikuwa vimekoma Hawa ndio wafalme wa nchi hii, wana wa Israeli waliowapiga, walipoichukua nchi yao, iwe yao wenyewe ng'ambo ya huko ya Yordani upande wa maawioni kwa jua toka mto wa Arnoni mpaka milimani kwa Hermoni, nayo nyika hiyo yote iliyoko upande wa maawioni kwa jua: Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekaa Hesiboni na kutawala toka Aroeri ulioko kwenye mto wa Arnoni kuanzia mle mtoni katikati kufikia nusu ya Gileadi mpaka mto wa Yaboko, mpaka wa wana wa Amoni uliko. Aliitawala nayo nyika kufikia upande wa maawioni kwa jua wa bahari ya Kineroti mpaka upande wa maawioni kwa jua wa bahari ya nyikani, ndiyo Bahari ya Chumvi, ukifuata njia ya kwenda Beti-Yesimoti, tena kusini chini ya matelemko ya Pisiga. Tena mipaka ya Ogi, mfalme wa Basani, aliyekuwa wa masao ya wale Majitu; naye alikuwa anakaa Astaroti na Edirei; aliitawala milima ya Hermoni na Salka na Basani yote mpaka kwenye mipaka ya Wagesuri na ya Wamakati na nusu ya Gileadi mpaka kwenye mipaka ya Sihoni, mfalme wa Hesiboni. Mose, mtumishi wa Bwana, na wana wa Isiraeli waliwapiga, nazo nchi zao Mose, mtumishi wa Bwana, akazigawia wao wa Rubeni na wa Gadi nao walio nusu ya shina la Manase, ziwe nchi zao. Nao hawa ndio wafalme, Yosua na wana wa Isiraeli waliowapiga ng'ambo ya huku ya Yordani inayoelekea baharini toka Baali-Gadi ulioko katika bonde la Libanoni mpaka kwenye ile milima mitupu inayoendelea hata Seiri; nchi hiyo Yosua akaigawia mashina ya Waisiraeli, iwe yao wenyewe, kama walivyogawanyika, wakae milimani na katika nchi ya tambarare na nyikani, hata kwenye matelemko na mbuga, nako kusini kwao Wahiti na Waamori na Wakanaani na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi: Mfalme wa Yeriko mmoja, mfalme wa Ai ulioko upande wa Beteli mmoja, mfalme wa Yerusalemu mmoja, mfalme wa Heburoni mmoja, mfalme wa Yarmuti mmoja, mfalme wa Lakisi mmoja, mfalme wa Egloni mmoja, mfalme wa Gezeri mmoja, mfalme wa Debiri mmoja, mfalme wa Gederi mmoja, mfalme wa Horma mmoja, mfalme wa Aradi mmoja, mfalme wa Libuna mmoja, mfalme wa Adulamu mmoja, mfalme wa Makeda mmoja, mfalme wa Beteli mmoja, mfalme wa Tapua mmoja, mfalme wa Heferi mmoja, mfalme wa Afeki mmoja, mfalme wa Saroni mmoja, mfalme wa Madoni mmoja, mfalme wa Hasori mmoja, mfalme wa Simuroni-Meroni mmoja, mfalme wa Akisafu mmoja, mfalme wa Taanaki mmoja, mfalme wa Megido mmoja, mfalme wa Kedesi mmoja, mfalme wa Yokinamu wa Karmeli mmoja, mfalme wa Dori milimani kwa Dori mmoja, mfalme wa makabila ya Gilgali mmoja, mfalme wa Tirsa mmoja, wafalme hawa wote ni 31. Yosua alipokuwa mzee mwenye siku nyingi, Bwana akamwambia: Wewe umekwisha kuwa mzee mwenye siku nyingi, nazo nchi zilizosalia uchukuliwa ni nyingi bado. Nazo nchi zilizosalia ni hizi: majimbo yote ya Wafilisti na Gesuri nzima toka mto wa Sihori ulioko upande wa Misri mpaka kwenye mipaka ya Ekroni kaskazini; kwani nchi hizo huhesabiwa kuwa za Wakanaani. Nao wakuu wa Wafilisti ni hawa watano: Wa Gaza na Wa Asdodi na wa Askaloni na wa Gati na wa Ekroni. Tena Waawi walioko kusini, tena nchi nzima ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni mpaka Afeki hata kwenye mipaka ya Waamori. Tena nchi ya Wagebali na ya Libanoni yote upande wa maawioni kwa jua toka Baali-Gadi chini ya milima ya Hermoni, mpaka ufike Hamati. Wote wakaao milimani toka Libanoni mpaka Misirefoti-Maimu, wale Wasidoni wote nitawafukuza wote mbele ya wana wa Isiraeli; wewe nchi hizi zigawie tu Waisiraeli na kuzipigia kura, ziwe fungu lao, kama nilivyokuagiza. Sasa nchi hizi zigawanyie yale mashina tisa na nusu ya Manase, ziwe mafungu yao! Nusu yake nyingine wamekwisha kuyachukua mafungu yao pamoja nao wa Rubeni na wa Gadi, Mose aliyowapa ng'ambo ya huko ya Yordani upande wa maawioni kwa jua; wameyachukua sawasawa, kama Mose, mtumishi wa Bwana, alivyowapa: toka Aroeri ulioko mtoni kwa Arnoni nao ule mji uliomo katikati ya mto na nchi ya tambarare yote ya Medeba mpaka Diboni. Nayo miji yote ya Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyetawala mle Hesiboni mpaka kwenye mipaka ya wana wa Amoni. Tena Gileadi nazo nchi za Gesuri na za Makati na milima yote ya Hermoni na Basani nzima mpaka Salka. Nchi zote za Basani zilizo za ufalme wa Ogi aliyetawala mle Astaroti na Edirei, ni yule aliyekuwa wa masao ya wale Majitu, Mose aliowapiga na kuwafukuza. Lakini wana wa Isiraeli hawakuwafukuza Wagesuri na Wamakati, nao Wagesuri na Wamakati wakapata kukaa katikati ya Waisiraeli hata siku hii ya leo. Wao na shina la Lawi tu Mose hakuwapa fungu, liwe lao, kwa maana ng'ombe za tambiko za kuchomwa motoni za Bwana Mungu wa Isiraeli ndizo zilizokuwa fungu lao, kama alivyowaambia. Mose aliwapa wao wa shina la Rubeni nchi ya kuzigawanyia koo zao. Mpaka wao ulianza Aroeri ulioko kwenye kijito cha Arnoni pamoja na ule mji ulioko mtoni katikati, ukaiingia nchi yote ya tambarare karibu ya Medeba na Hesiboni pamoja na miji yake yote iliyoko katika nchi ya tambarare: Diboni na Bamoti-Baali na Beti-Baali-Meoni, na Yasa na Kedemoti na Mefati, na Kiriataimu na Sibuma na Sereti-Sahari ulioko juu ya mlima wa hilo bonde, na Beti-Peori na matelemko ya Pisiga na Beti-Yesimoti na miji yote ya hiyo nchi ya tambarare. Tena ufalme wote wa Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyetawala mle Hesiboni; ni yule, Mose aliyempiga pamoja na wakuu wa Wamidiani, Ewi na Rekemu na Suri na Huri na Reba, ndio wakuu wa Sihoni waliokaa katika nchi hiyo. Hata mwaguaji Bileamu, mwana wa Beori, wana wa Isiraeli walimwua kwa upanga pamoja na wengine waliouawa nao. Mpaka mwingine wa wana wa Rubeni ulikuwa mto wa Yordani. Huu ulikuwa mpaka wa fungu lao wana wa Rubeni la kuzigawanyia koo zao ile miji pamoja na mitaa yao. Nao wa shina la Gadi, wale wana wa Gadi, Mose aliwapa nchi ya kuzigawanyia koo zao. Mpaka wao ulikuwa huu: Yazeri na miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya wana wa Amoni mpaka Aroeri unaoelekea Raba. Tena kutoka Hesiboni mpaka Ramati-Misipe na Betonimu, tena toka Mahanaimu kufika kwenye mpaka wa Debiri. Tena bondeni Beti-Haramu na Beti-Nimura na Sukoti na Safoni na kipande kilichosalia cha ufalme wa Sihoni, mfalme wa Hesiboni; hapo mto wa Yordani ulikuwa mpaka hata mwisho wa bahari ya Kinereti ng'ambo ya huko ya Yordani ya upande wa maawioni kwa jua. Hili ni fungu lao wana wa Gadi la kuzigawanyia koo zao. Nao waliokuwa nusu ya shina la Manase Mose aliwapa nchi, ikawa yao waliokuwa nusu ya wana wa Manase ya kuzigawanyia koo zao. Mpaka wao ulianza Mahanaimu, ukachukua Basani nzima, ndiyo nchi yote ya Ogi, mfalme wa Basani, pamoja na vijiji vyote vya Mahema ya Yairi vilivyokuwako kule Basani, pamoja ni miji 60. Tena mpaka wao ukachukua nusu ya Gileadi na Astaroti na Edirei, ile miji ya kifalme ya Ogi kule Basani. Nchi hii ilikuwa yao wana wa Makiri, mwana wa Manase, waliokuwa nusu tu ya wana wa Makiri, ya kuzigawanyia koo zao. Hizi ndizo nchi, Mose alizowapa, ziwe mafungu yao katika nyika za Moabu ng'ambo ya huko ya Yordani upande wa maawioni kwa jua, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili. Lakini wao wa shina la Lawi Mose hakuwapa fungu, liwe lao, kwani Bwana Mungu wa Isiraeli, yeye ni fungu lao, kama alivyowaambia. Hizi ndizo nchi, wana wa Isiraeli walizozipata katika nchi ya Kanaani kuwa mafungu yao; nao waliowagawanyia haya mafungu ni mtambikaji Elazari na Yosua, mwana wa Nuni, pamoja na wakuu wa baba za mashina ya wana wa Isiraeli. Waliyapata mafungu yao kwa kuyapigia kura, kama Bwana alivyoviagiza kinywani mwa Mose kwa ajili ya hayo mashina tisa na nusu ya Manase. Kwani yale mashina mawili na nusu ya lile shina moja Mose aliwapa mafugu yao ng'ambo ya huko ya Yordani, lakini Walawi hakuwapa fungu katikati yao. Kwani wana wa Yosefu walikuwa mashina mawili: Manase na Efuraimu, lakini Walawi hawakuwapa fungu katika nchi yao, walipata miji tu ya kukaa pamoja na malisho yao ya kulisha nyama wao wa kufuga na mahali pa kuwekea mapato yao. Kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, wana wa Isiraeli walivyovifanya walipojigawanyia nchi hiyo. Hapo, wana wa Yuda walipofika kwake Yosua kule Gilgali, Mkenizi Kalebu, mwana wa Yefune, akamwambia: Wewe unalijua lile neno, Mungu alilolisema kule Kadesi-Barnea kwa ajili yangu na kwa ajili yako. Mimi nilikuwa mwenye miaka 40, Mose, mtumishi wa Bwana, aliponituma kule Kadesi-Barnea kwenda kuipeleleza nchi hii, nami nikamletea habari za mambo ya huku, kama nilivyoyaona moyoni mwangu. Lakini ndugu zangu waliopanda pamoja nami wakaiyeyusha mioyo ya watu hawa, lakini mimi nilijishupaza kabisa kumfuata Bwana Mungu wangu. Siku hiyo Mose akaapa kwamba: Nchi hiyo, miguu yako iliyoikanyaga, itakuwa fungu lako, iwe yako na ya wanao kale na kale, kwa kuwa umejishupaza kabisa kumfuata Bwana Mungu wangu. Sasa tazama, Bwana amenikalisha uzimani, kama alivyosema, tangu hapo, alipomwambia Mose lile neno, miaka hii 45, Waisiraeli waliyoitembea nyikani, sasa leo hivi unaniona kuwa mwenye miaka 85. Na leo ningaliko mwenye nguvu kama siku hiyo, Mose aliponituma; nguvu zangu kama zilivyokuwa hapo, ndivyo, hizo nguvu zangu zilivyo na leo za kupiga vita, nipate kwenda na kurudi. Sasa nipe milima hiyo, Bwana aliyoitaja siku hiyo. Kwani mwenyewe ulisikia siku hiyo, ya kuwa wako Waanaki, ya kuwa iko nayo miji mikubwa yenye maboma. Labda Bwana atakuwa pamoja na mimi, nipate kuwafukuza, kama Bwana alivyosema. Ndipo, Yosua alipombariki Kalebu, mwana wa Yefune, akampa Heburoni, uwe fungu lake. Kwa hiyo Heburoni ukawa wake Mkenizi Kalebu, mwana wa Yefune, uwe fungu lake mpaka siku hii ya leo, kwa kuwa alijishupaza kabisa kumfuata Bwana Mungu wa Isiraeli. Kale jina lake Heburoni lilikuwa mji wa Arba aliyekuwa mkubwa kuwapita Waanaki wote. Siku zile nchi hii ikapata kutengemana, kwa kuwa vita vilikoma. Shina la wana wa Yuda kura ikalipata nchi za kuzigawanyia koo zao kwenye mpaka wa Edomu; mpaka wao wa kusini uliipita nyika ya Sini iliyokuwa mwisho wa upande wa kusini. Huo mpaka wao wa upande wa kusini ulianzia mwishoni kwa Bahari ya Chumvi kwenye pembe yake ielekeayo kusini. Kutoka kule kusini ulipita hapo pa kukwelea Akarabimu, ulipitia Sini, ulipanda tena upande wa kusini wa Kadesi-Barnea, ulipita Hesironi na kupanda tena Adari, ulizungukia Karka, ulifika Asimoni, kisha ulitokea kwenye mto wa Misri, mwisho ulitokea baharini. Huu ndio mpaka wenu wa kusini. Mpaka wa upande wa maawioni kwa jua ni Bahari ya Chumvi kuufikia mwisho wa Yordani. Nao mpaka wa upande wa kaskazini ulianzia hapo pembeni kwa bahari kwenye mwisho wa Yordani. Kutoka huko mpaka ulipanda Beti-Hogla, ulipitia Beti-Araba upande wake wa kaskazini, kisha mpaka uliupanda mwamba wa Bohani, mwana wa Rubeni. Kutoka Bondeni kwa Akori mpaka ulipanda Debiri, uligeukia kaskazini kufika Gilgali unaoelekea hapo pa kukwelea Adumimu ulioko kusini kwenye kijito; kisha mpaka ulipita penye maji ya Eni-Semesi na kutokea Eni-Rogeli (Chemchemi ya Wafua nguo). Kisha mpaka ulipanda katika bonde la Mwana wa Hinomu kufika kando kwao Wayebusi upande wao wa kusini, ni huko Yerusalemu; kisha mpaka ulipanda kufika juu ya mlima ulioko mbele ya Bonde la Hinomu upande wa baharini mwishoni kwa Bonde la Majitu upande wake wa kaskazini. Toka juu ya mlima huo mpaka uliendelea, ufike kwenye chemchemi ya maji ya Nefutoa, utokee kwenye miji ya mlima wa Efuroni; uliendelea tena kufika Bala, ndio Kiriati-Yearimu. Huko Bala mpaka uligeukia tena upande wa baharini kuufikia mlima wa Seiri, tena ulipita kando ya mlima wa Yearimu upande wake wa kaskazini, ndio Kesaloni; toka huko ulishuka Beti-Semesi, ufike Timuna. Toka huko mpaka uliendelea kando ya Ekroni upande wa kaskazini, kisha uliendelea kufika Sikroni, uliupita mlima wa Bala, utokee Yabuneli, nao mwisho wake mpaka ulikuwa hapo, ulipotokea baharini. Nao mpaka wa upande wa baharini ulikuwa Bahari Kubwa na nchi yake ya pwani. Hii ilikuwa mipaka ya kuzizunguka nchi za wana wa Yuda za kuzigawanyia koo zao. Kalebu, mwana wa Yefune, akampa fungu katikati ya wana wa Yuda, liwe lake kwa hivyo, Bwana alivyomwambia Yosua; ni mji wa Arba, baba yao Waanaki, ndio Heburoni. Huko Kalebu akafukuza wana watatu wa Anaki, Sesai na Ahimani na Talmai, waliozaliwa na Anaki. Toka huko akawaendea wenyeji wa Debiri, nalo jina la Debiri lilikuwa kale Kiriati-Seferi. Hapo Kalebu akasema: Atakayeupiga Kiriati-Seferi na kuuteka nitampa mtoto wangu Akisa kuwa mkewe. Otinieli, mwana wa Kenazi, ndugu yake Kalebu, alipouteka, akampa mtoto wake Akisa kuwa mkewe. Ikawa, huyu alipofikia kwake akamhimiza mumewe kuomba shamba kwa baba yake Kalebu; basi, Akisa aliposhuka katika punda, Kalebu akamwuliza: Unataka nini? Naye akamwambia: Nipe tunzo la kunibariki! Kwa kuwa umenipeleka katika nchi ya kusini, nipe nazo mboji za maji! Ndipo, alipompa zile mboji zilizokuwa upande wa juu, nazo zilizokuwa upande wa chini. Hizi ndizo nchi za shina la wana wa Yuda za kuzigawanyia koo zao, ziwe mafungu yao: kwenye mwisho wa nchi ya shina la wana wa Yuda kuuelekea mpaka wa Edomu upande wa kusini kulikuwa na miji hii: Kabuseli na Ederi na Yaguri, na Kina na Dimona na Adada, na Kedesi na Hasori na Itinani, Zifu na Telemu na Baloti, na Hasori-Hadata na Kerioti-Hesironi, ndio Hasori. Amamu na Sema na Molada, na Hasari-Gada na Hesimoni na Beti-Peleti, na Hasari-Suali na Beri-Seba na Biziotia, Bala na Iyimu na Esemu, na Eltoladi na Kesili na Horma, na Siklagi na Madimana na Sanisana, Lebaoti na Silihimu na Aini na Rimoni; miji hii yote pamoja ni 29 pamoja na mitaa yao. Katika nchi ya tambarare: Estaoli na Sora na Asina, na Zanoa na Eni-Ganimu, Tapua na Enamu, Yarmuti na Adulamu, Soko na Azeka, na Saraimu na Aditaimu na Gedera na Gederotaimu; ni miji 14, pamoja na mitaa yao. Senani na Hadaa na Migidali-Gadi, na Dilani na Misipe na Yokiteli, Lakisi na Boskati na Egloni, na Kaboni na Lamasi na Kitilisi, na Gederoti, Beti-Dagoni na Nama na Makeda; ni miji 16 pamoja na mitaa yao. Libuna na Eteri na Asani, Ifuta na Asina na Nesibu, na Keila na Akizibu na Maresa; ni miji 9 pamoja na mitaa yao. Ekroni na vijiji vyake na mitaa yake. Toka Ekroni upande wa baharini miji yote iliyoko kando ya Asdodi pamoja na mitaa yao. Asdodi na vijiji vyake na mitaa yake, Gaza pamoja na vijiji vyake na mitaa yake mpaka kwenye mto wa Misri, nao mpaka wake ni Bahari Kubwa. Tena milimani: Samiri na Yatiri na Soko, na Dana na Kiriati-Sana, ndio Debiri, na Anabu na Estemo na Animu, na Goseni na Holoni na Gilo; ni miji 11 pamoja na mitaa yao. Arabu na Duma na Esani, Yanumu na Beti-Tapua na Afeka, na Humuta na Kiriati-Arba, ndio Heburoni, na Siori; ni miji 9 pamoja na mitaa yao. Maoni, Karmeli na Zifu na Yuta, na Izireeli na Yokidamu na Zanoa, Kaini, Gibea na Timuna; ni miji 10 pamoja na mitaa yao. Halihuli, Beti-Suri na Gedori, na Marati na Beti-Anoti na Eltekoni; ni miji 6 pamoja na mitaa yao. Kiriati-Baali, ndio Kiriati-Yearimu, na Raba; ni miji 2 pamoja na mitaa yao. Nyikani: Beti-Araba, Midini na Sekaka, na Nibusani na Mji wa Chumvi na Engedi ni miji 6 pamoja na mitaa yao. Lakini Wayebusi, ndio wenyeji wa Yerusalemu, wana wa Yuda hawakuweza kuwafukuza; kwa hiyo Wayebusi wakakaa pamoja na wana wa Yuda mle Yerusalemu mpaka siku hii ya leo. Wana wa Yosefu kura ikawapatia nchi toka Yordani karibu ya Yeriko, nao mpaka wa maawioni kwa jua ulikuwa yale maji ya Yeriko, ulichukua nayo nyika inayopanda kutoka Yeriko mpaka mlimani kwa Beteli. Mpaka ulipotoka Beteli ulifika Luzi, tena uliendelea, ufike mpakani kwa Waarki hata Ataroti. Toka huko ulitelemka upande wa baharini kuufikia mpaka wa Wayafuleti hata mpaka wa Beti-Horoni wa chini mpaka Gezeri; mwisho ulitokea baharini. Wana wa Yosefu, Manase na Efuraimu, wakazipata nchi hizi, ziwe mafungu yao. Nchi, wana wa Efuraimu walizozipata za kuzigawanyia koo zao, mipaka yao ni hii: mpaka wa fungu lao wa maawioni kwa jua ulianzia Ataroti-Adari, ulifika Beti-Horoni wa juu. Toka huko mpaka ulikwenda kufika baharini. Upande wa kaskazini mpaka ulianzia Mikimetati, ulizunguka kwenda upande wa maawioni kwa jua, ufike Tanati-Silo, kisha ulipitia Yonoha upande wake wa maawioni kwa jua. Toka Yanoha ulitelemka kufika Ataroti na Nara, kisha uligusa Yeriko na kutokea Yordani. Tena kutoka Tapua mpaka ulikwenda upande wa baharini, ufike kwenye mto wa Kana, kisha ulitokea baharini. Nchi hizi zilikuwa fungu la shina la wana wa Efuraimu la kuzigawanyia koo zao. Tena wana wa Efuraimu walikuwa na miji waliyowekewa katikati ya fungu la wana wa Manase, nayo miji hiyo ilikuwa pamoja na mitaa yao. Lakini hawakuwafukuza Wakanaani waliokaa Gezeri; kwa hiyo Wakanaani wakakaa katikati ya Waefuraimu mpaka siku hii ya leo, lakini hawakuwa na budi kuwafanyizia kazi za kitumwa Kisha shina la Manase likapigiwa kura, kwani yeye alikuwa mwana wa kwanza wa Yosefu. Naye Manase mwanawe wa kwanza alikuwa Makiri, babake Gileadi; kwa kuwa huyu alikuwa mtu wa kupiga vita, alipewa Gileadi na Basani. Kisha wana wa Manase waliosalia wakapata mafungu yao ukoo kwa ukoo, wana wa Abiezeri na wana wa Heleki na wana wa Asirieli na wana wa Sekemu na wana wa Heferi na wana wa Semida; hawa ndio wana wa kiume wa Manase, mwana wa Yosefu, kwa koo zao. Lakini Selofuhadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na wana wa kiume, ila wa kike tu, nayo haya ndiyo majina ya wanawe wa kike: Mala na Noa, Hogla, Milka na Tirsa. Hawa wakamtokea mtambikaji Elazari na Yosua, mwana wa Nuni, na wakuu kwamba: Bwana alimwagiza Mose kutupa sisi fungu katikati ya waumbu zetu, liwe letu! Kwa agizo hilo la Bwana akawapa fungu katikati ya ndugu za baba yao, liwe lao. Kwa hiyo Manase akagawiwa na kura mafungu kumi pasipo kuzihesabu nchi za Gileadi na za Basani zilizoko ng'ambo ya huko ya Yordani, kwani wana wa kike wa Manase waligawiwa mafungu, yawe yao katikati ya wanawe wa kiume, nayo nchi ya Gileadi ikawa yao wana wa Manase waliosalia. Nao mpaka wa Manase ulitoka kwa Aseri, ukaja Mikimetati unaoelekea Sikemu; huko uligeukia kuumeni kufika kwa wenyeji wa Eni-Tapua. Nchi ya Tapua ilikuwa yake Manase, lakini mji wa Tapua uliokuwa mpakani ulikuwa wao wana wa Efuraimu. Kisha mpaka ulitelemka kwenye kijito cha Kana upande wa kusini wa hicho kijito; huko iko miji ya Waefuraimu katikati ya miji ya Manase. Kisha mpaka wa Manase uliendelea upande wa kaskazini wa hicho kijito, hata utokee baharini. Upande wa kusini ulikuwa wa Efuraimu, nao upande wa kaskazini ulikuwa wa Manase; nayo bahari ilikuwa mpaka: upande wake wa kaskazini walipakana na Aseri, nao upande wa maawioni kwa jua walipakana na Isakari. Tena Manase alipata kwa Isakari na kwa Aseri miji hii: Beti-Seani pamoja na vijiji vyake na Ibilamu pamoja na vijiji vyake na wenyeji wa Dori pamoja na vijiji vyake na wenyeji wa Endori pamoja na vijiji vyake na wenyeji wa Taanaki pamoja na vijiji vyake na wenyeji wa Megido pamoja na vijiji vyake, ni ile nchi yenye vilima vitatu. Lakini wana wa Manase hawakuweza kuwafukuza wenyeji wa hiyo miji; ndivyo, Wakanaani walivyopata kukaa kwanza katika nchi hii. Lakini Waisiraeli walipopata nguvu wakawashurutisha Wakanaani kuwafanyia kazi za kitumwa, lakini kufukuza hawakuwafukuza. Kisha wana wa Yosefu wakamwambia Yosua kwamba: Mbona umetupigia kura mara moja tu na kutupatia fungu moja tu, liwe letu, nasi tu watu wengi, kwa kuwa Bwana ametubariki mpaka sasa! Yosua akawaambia: Kama ninyi m watu wengi, haya pandeni kwenye misitu kuikata, mjipatie pa kukaa huko katika nchi ya Waperizi na katika nchi ya Majitu, ikiwa milima ya Efuraimu inawasonga, isiwatoshe. Ndipo, wana wa Yosefu waliposema: Milima hii haitutoshi kweli; lakini Wakanaani wote wanaokaa bondeni kwa Beti-Seani na katika vijiji vyake nao wanaokaa bondeni kwa Izireeli wako na magari ya chuma ya kupigia vita. Ndipo, Yosua alipowaambia wao wa mlango wa Yosefu, wao Wamanase na Waefuraimu, kwamba: Ninyi mkiwa watu wengi wenye nguvu kubwa, hamtapata kwa kura nchi moja tu, iwe yenu. Kwani nchi yote ya milima nayo ni yako; kweli ni yenye misitu, lakini huko ndiko, utakakoweza kujipatia pa kukaa wa kuikata, kwani mwisho, itakapotokea kuwa wazi, itakuwa yenu. Kwani Wakanaani mtawafukuza, ijapo wawe wenye magari ya chuma ya kupigia vita, tena ijapo nguvu zao zaidi. Mkutano wote wa wana wa Isiraeli ukakusanyika huko Silo, wakapanga huko lile Hema la Mkutano, kwani nchi hii ilikuwa imekwisha kushindwa nao. Lakini kwao wana wa Isiraeli walikuwako mashina saba wasiopata bado mafungu yao ya nchi. Ndipo, Yosua alipowaambia wana wa Isiraeli: Mpaka lini ninyi mtailegeza mikono yenu, msiende kuichukua nchi hii, Bwana Mungu wa baba zenu aliyowapa? Haya! Jichagulieni kila shina watu watatu, niwatume, waondoke kwenda katika nchi hiyo, waiandike hiyo itakayokuwa fungu lao! Kisha watakaporudi kwangu, waigawanye, itoke mafungu saba, Wayuda wakiushika mpaka wao upande wa kusini nao wa mlango wa Yosefu wakiushika wao mpaka upande wa kaskazini. Ninyi mtakapokwisha kuiandika nchi, itoke mafungu saba, mniletee hapa huo mwandiko! Ndipo, nitakapowapigia kura hapa machoni pa Bwana Mungu wetu. Kwani Walawi hawatapata fungu katikati yenu, kwani utambikaji wa Bwana ndio fungu lao; nao Wagadi na Warubeni na nusu ya Wamanase wamekwisha kuyachukua mafungu yao ng'ambo ya huko ya Yordani upande wa maawioni kwa jua, aliyowapa Mose, mtumishi wa Bwana. Ndipo, watu wale walipoondoka kwenda zao, nao waliokwenda kuiandika nchi Yosua akawaagiza kwamba: Nendeni kuzunguka katika nchi hiyo na kuiandika! Kisha rudini kwangu! Ndipo, nitakapowapigia kura machoni pa Bwana hapa Silo. Wale watu wakaenda, wakapita po pote katika hizo nchi, wakaziandika katika kitabu, mji kwa mji, zipate kutokea kuwa mafungu saba, kisha wakarudi makambini kwa Yosua huko Silo. Ndipo, Yosua alipowapigia kura huko Silo machoni pa Bwana; ndivyo, Yosua alivyowagawanyia wale wana wa Isiraeli hizo nchi, wayapate mafungu yao. Ikatokea kura ya shina la wana wa Benyamini ya kuzigawanyia koo zao, nayo nchi, kura iliyowapatia, ilikuwa katikati ya wana wa Yuda na wana wa Yosefu. Mpaka wao wa upande wa kaskazini ulitoka mtoni kwa Yordani, kisha mpaka ulipanda kandokando ya Yeriko upande wake wa kaskazini, tena uliendelea kupanda milimani upande wa baharini, utokee katika nyika ya Beti-Aweni. Toka huko mpaka uliendelea kufika Luzi, kando ya Luzi kuelekea kusini, nao Luzi ndio Beteli; kisha mpaka ulishukia Ataroti-Adari katika ule mlima ulioko upande wa kusini wa Beti-Horoni wa chini. Kisha mpaka uliendelea na kugeuka upande wake wa baharini, uelekee kusini toka mlima huo unaoelekea Beti-Horoni upande wa kusini, utokee Kiriati-Baali, ndio Kiriati-Yearimu ulio mji wa wana wa Yuda. Huu ndio upande wake wa kuelekea baharini. Nao upande wake wa kuelekea kusini ulianza pembeni kwa Kiriati-Yearimu; mpaka ulipotoka huko uliendelea upande wa baharini kufika kwenye chemchemi ya maji ya Nefutoa. Toka huko mpaka ulitelemka kufika pembeni kwa mlima ule unaoelekea bondeni kwa mwana wa Hinomu ulioko upande wa kaskazini wa Bonde la Majitu, ulishuka Bondeni kwa Hinomu kando kwao Wayebusi upande wao wa kusini, tena uliendelea kushuka Eni-Rogeli. Toka huko mpaka uliendelea na kugeukia kaskazini na kutoka Eni-Semesi, ulitokea Geliloti unaoelekea hapo pa kukwelea Adumimu, kisha ulishuka kwenye mwamba wa Bohani, mwana wa Rubeni. Toka huko mpaka uliendelea na kupita upande wa kaskazini kando ya kilima kinachoelekea Araba, kisha ulitelemkia hapo Araba; kisha mpaka uliendelea na kupita kando ya Beti-Hogla upande wa kaskazini, upate kutokea pembeni kwa Bahari ya Chumvi upande wake wa kaskazini kwenye mwisho wa kusini wa Yordani. Huu ndio mpaka wa kusini. Lakini Yordani ulikuwa mpaka wake wa upande wa maawioni kwa jua. Hili lilikuwa fungu lao wana wa Benyamini la kuzigawanyia koo zao, mipaka yake ilivyolizunguka. Miji ya shina la wana wa Benyamini ya kuzigawanyia koo zao ilikuwa: Yeriko na Beti-Hogla na Emeki-Kesisi, na Beti-Araba na Semaraimu na Beteli, na Awimu na Para na Ofura, na Kefari-Amoni na Ofuni na Geba; ndio miji 12 pamoja na mitaa yao. Gibeoni na Rama na Beroti, na Misipe na Kefira na Mosa, na Rekemu na Iripeli na Tarala, na Sela, na Elefu na Yebusi, ndio Yerusalemu, Gibeati, Kiriati, ndio miji 14 pamoja na mitaa yao. Hili lilikuwa fungu lao wana wa Benyamini la kuzigawanyia koo zao. Kura ya pili iliyotokea ilikuwa ya shina la wana wa Simeoni ya kuzigawanyia koo zao; nalo fungu lao lilikuwa katikati ya wana wa Yuda. Hilo fungu, walilolipata, liwe lao, lilikuwa: Beri-Seba na Seba na Molada, na Hasari-Suali na Bala na Esemu, na Eltoladi na Betuli na Horma, na Siklagi na Beti-Markaboti na Hasari-Susa, na Beti-Lebaoti na Saruheni; ndio miji 13 na mitaa yao. Aini, Rimoni na Eteri na Asani, ndio miji 4 na mitaa yao. Tena mitaa yote pia iliyoizunguka miji hii mpaka Bala-Beri ulio Rama wa kusini. Hii lilikuwa fungu lao wana wa Simeoni la kuzigawanyia koo zao. Hili fungu la wana wa Simeoni lilichukuliwa katika nchi, wana wa Yuda waliyopimiwa, kwani fungu lao wana wa Yuda lilikuwa kubwa zaidi, wasilikae lote. Kwa hiyo wana wa Simeoni walipata fungu lao katikati ya fungu lao wale. Kura ya tatu iliyotokea ilikuwa ya wana wa Zebuluni ya kuzigawanyia koo zao, nao mpaka wa fungu lao ulifika hata Saridi. Toka huko mpaka wao ulipanda upande wa baharini kufika Marala na kugusa Dabeseti, kisha ulikigusa kijito kile kinachopita mbele ya Yokinamu. Tena toka Saridi mpaka uligeukia upande wa mashariki, ndio maawioni kwa jua, ufike kwenye mpaka wa Kisiloti-Tabori, toka huko ulifika Daberati na kupanda Yafia. Toka huko uliendelea upande wa mashariki, ndio wa maawioni, ufike Gati-Heferi na Eti-Kasini, utokee Rimoni na kufika hata Nea. Kisha mpaka uliuzunguka mji huu upande wa kaskazini wa Hanatoni, upate kutokea bondeni kwa Ifuta-Eli, kuliko na miji ya Katati na Nahalali na Simuroni na Idala na Beti-Lehemu; miji ilikuwa 12 na mitaa yao. Hili lilikuwa fungu lao wana wa Zebuluni la kuzigawanyia koo zao ile miji pamoja na mitaa yao. Kura ya nne iliyotokea ilikuwa ya wana wa Isakari ya kuzigawanyia koo zao. Mpaka wao ulichukua Izireeli na Kesuloti na Sunemu, na Hafaraimu na Sioni na Anaharati, na Rabiti na Kisioni na Abesi, na Remeti na Eni-Ganimu na Eni-Hada na Beti-Pasesi. Kisha mpaka uligusa Tabori na Sahasima na Beti-Semesi, kisha mpaka wao ulitokea Yordani; miji ilikuwa 16 pamoja na mitaa yao. Hili lilikuwa fungu la shina la wana wa Isakari la kuzigawanyia koo zao ile miji pamoja na mitaa yao. Kura ya tano iliyotokea ilikuwa ya shina la wana wa Aseri ya kuzigawanyia koo zao. Mpaka wao ulichukua Helkati na Hali na Beteni na Akisafu, na Alameleki na Amadi na Misali; kisha mpaka uligusa Karmeli upande wa baharini na Sihori-Libunati. Toka huko mpaka uligeukia upande wa maawioni kwa jua kufika Beti-Dagoni, kisha uligusa Zebuluni na bonde la Ifuta-Eli upande wake wa kaskazini, ulipita Beti-Emeki na Nieli, upate kutokea Kabuli kushotoni kwake. Kisha ulichukua Eburoni na Rehobu na Hamoni na Kana, uufikie ule mji mkubwa wa Sidoni. Huko mpaka uligeuka tena kufika Rama, hata mji wa Tiro uliokuwa na boma, kisha mpaka uligeuka tena kufika Hosa, upate kutokea baharini upande wa nchi ya Akizibu. Hata Uma na Afeki na Rehobu ilikuwa ya huko. Miji ilikuwa 22 pamoja na mitaa yao. Hili lilikuwa fungu la shina la wana wa Aseri la kuzigawanyia koo zao ile miji pamoja na mitaa yao. Kura ya sita iliyotokea ilikuwa ya wana wa Nafutali ya kuzigawanyia koo zao. Mpaka wao ulitoka Helefu kwenye mvule wa Sananimu, ulichukua Adami-Nekebu na Yabuneli, hata Lakumu, utokee Yordani. Tena mpaka uligeukia upande wa baharini, ufike Azinoti-Tabori; ulipotoka huko ulikwenda Hukoki, upande wa kusini uligusa Zebuluni, nao upande wa baharini uligusa Aseri, nao upande wa maawioni kwa jua uligusa Yuda kwenye Yordani. Miji yenye maboma ilikuwa: Sidimu, Seri na Hamati, Rakati na Kinereti (Genezareti), na Adama na Rama na Hasori, na Kedesi na Edirei na Eni-Hasori, na Ironi na Migidali-Eli, Horemu na Beti-Anati na Beti-Semesi; miji ilikuwa 19 pamoja na mitaa yao. Hili lilikuwa fungu la shina la wana wa Nafutali la Kuzigawanyia koo zao ile miji pamoja na mitaa yao. Kura ya saba iliyotokea ya shina la wana wa Dani ya kuzigawanyia koo zao. Mpaka wa fungu lao ulichukua Sora na Estaoli na Iri-Semesi, na Salabini na Ayaloni na Itila, na Eloni na Timuna na Ekroni, na Elteke na Gibetoni na Bala, na Yudi na Bene-Beraki na Gati-Rimoni, na Me-arkoni na Rakoni nayo nchi ielekeayo Yafo; huko ndiko, mpaka wa wana wa Dani ulikotokea. Halafu wana wa Dani walikwenda kupigana na mji wa Lesemu, wakauteka, wakawapiga waliokuwamo kwa ukali wa panga, kisha wakauchukua, wakakaa humo, wakaacha kuuita Lesemu wakauita Dani kwa jina la baba yao Dani. Hili lilikuwa fungu la shina la wana wa Dani la kuzigawanyia koo zao ile miji pamoja na mitaa yao. Wana wa Isiraeli walipokwisha kuigawanya nchi hii na kujipatia mafungu yao katika mipaka yake wakampa Yosua, mwana wa Nuni, fungu lake katikati yao. Kwa kuagizwa na Bwana wakampa huo mji, alioutaka, ndio Timunati-Sera milimani kwa Efuraimu, kisha akaujenga mji huu, akakaa humo. Haya ndiyo mafungu, mtambikaji Elazari na Yosua, mwana wa Nuni, na wakuu wa milango ya baba zao waliyowagawanyia mashina ya wana wa Isiraeli kwa kuyapigia kura huko Silo machoni pa Bwana pa kuliingilia Hema la Mkutano; ndivyo, walivyomaliza kuigawanya nchi hii. Kisha Bwana akamwambia Yosua kwamba: Waambie wana wa Isiraeli kwamba: Jipatieni ile miji ya kuikimbilia, niliyowaambia kinywani mwa Mose, mwuaji apate kuikimbilia, kama hakumpiga mwenziwe na kumwua kwa kusudi wala kwa kujua, mpate kuikimbilia na kumkimbia atakayeilipiza hiyo damu. Kama anakimbilia mmojawapo hiyo mji, asimame pa kuliingilia lango la mji na kusema masikioni pa wazee wa miji huo manza zake, alizozikora, kisha sharti wampokee mjini mwao na kumpa mahali pa kukaa kwao. Kama mwenye kuilipiza ile damu anamfuata upesi, wasimtoe yule mwuaji na kumtia mkononi mwake, kwa kuwa alimpiga mwenziwe pasipo kujua, wala hakumchukia tangu kale. Naye atakaa humo mjini, mpaka atakaposimamishwa mbele ya mkutano, apate kuhukumiwa, tena mpaka mtambikaji mkuu wa siku zile atakapokufa, kisha yule mwuaji atapata kurudi na kuingia mjini kwao na nyumbani mwao mlemle mjini, alimotoka na kukimbia. Ndipo, walipoeua Kedesi katika nchi ya Galili milimani kwa Nafutali na Sikemu milimani kwa Efuraimu na Kiriati-Arba, ndio Heburoni, milimani kwa Yuda. Tena ng'ambo ya huko ya Yordani upande wa Yeriko wa Maawioni kwa jua wakatoa kwa shina la Rubeni mji wa Beseri ulioko nyikani juu mlimani panapokwenda sawa, tena Ramoti wa Gileadi kwa shina la Gadi na Golani wa Basani kwa shina la Manase. Hii ndiyo miji iliyowekewa wana wote wa Isiraeli nao wageni waliokaa ugenini kwao ya kuikimbilia; mtu ye yote asiyemwua mwenziwe kwa kusudi asiuawe na mkono wake mwenye kuilipiza hiyo damu, mpaka asimamishwe mbele ya mkutano. Kisha wakuu wa milango ya Walawi wakamjia mtambikaji Elazari na Yosua, mwana wa Nuni, na wakuu wa milango ya mashina ya wana wa Isiraeli, wakawaambia huko Silo katika nchi ya Kanaani kwamba: Bwana aliagiza kinywani mwa Mose kutupa sisi miji ya kukaa pamoja na malisho yao ya nyama wetu wa kufuga. Kwa hiyo wana wa Isiraeli wakawatolea Walawi kwa kuagizwa na Bwana katika mafungu yao miji hii pamoja na malisho yao: Koo za Wakehati zilipopigiwa kura, wana wa mtambikaji Haroni waliokuwa katika hawa Walawi walipata miji 13 kwa shina la Yuda na kwa shina la Simeoni na kwa shina la Benyamini. Nao wana wa Kehati waliosalia walipopigiwa kura walipata miji 10 kwa koo za shina la Efuraimu na kwa shina la Dani na kwa nusu ya shina la Manase. Nao wana wa Gersoni walipopigiwa kura walipata miji 13 kwa koo za shina la Isakari na kwa shina la Aseri na kwa shina la Nafutali na kwa nusu ya shina la Manase kule Basani. Nao wana wa Merari walipata miji 12 ya kuzigawanyia koo zao kwa shina la Rubeni na kwa shina la Gadi na kwa shina la Zebuluni. Miji hii ndiyo, wana wa Isiraeli waliyowapa Walawi pamoja na malisho yao kwa kuwapigia kura, kama Bwana alivyoviagiza kinywani mwa Mose. Kwa shina la wana wa Yuda na kwa shina la wana wa Simeoni waliwapa Walawi miji hii, waliyoita kwa majina yao. Wana wa Haroni walipigiwa kura ya kwanza ya koo za Kehati katika wana wa Lawi. Wakawapa Kiriati wa Arba aliyekuwa baba yake Anaki, ndio Heburoni ulioko milimani kwa Yuda pamoja na malisho yake yaliyouzunguka. Lakini mashamba yake pamoja na mitaa yake walikuwa wamempa Kalebu, mwana wa Yefune, yawe mali zake za kuzishika. Lakini wana wa mtambikaji Haroni waliwapa huo mji wa Heburoni, uliokuwa wa kukimbilia wauaji, pamoja na malisho yake, tena Libuna pamoja na malisho yake, na Yatiri pamoja na malisho yake na Estemoa pamoja na malisho yake, na Holoni pamoja na malisho yake na Debiri pamoja na malisho yake, na Aini pamoja na malisho yake na Yuta pamoja na malisho yake, Beti-Semesi pamoja na malisho yake, ndio miji 9 kwa mashina haya mawili. Tena kwa shina la Benyamini: Gibeoni pamoja na malisho yake na Geba pamoja na malisho yake, na Anatoti pamoja na malisho yake na Almoni pamoja na malisho yake, ndio miji 4. Miji yote ya wana wa Haroni waliokuwa watambikaji ilikuwa miji 13 pamoja na malisho yao. Nazo koo za wana wa Kehati waliokuwa Walawi, ndio wana wa Kehati waliosalia, walipopigiwa kura yao walipata miji kwa shina la Efuraimu. Wakawapa Sikemu uliokuwa wa kukimbilia wauaji pamoja na malisho yake milimani kwa Efuraimu na Gezeri pamoja na malisho yake, na Kibusaimu pamoja na malisho yake na Beti-Horoni pamoja na malisho yake, ndio miji 4. Tena kwa shina la Dani: Elteke pamoja na malisho yake na Gibetoni pamoja na malisho yake, na Ayaloni pamoja na malisho yake na Gati-Rimoni pamoja na malisho yake, ndio miji 4. Tena kwa nusu ya shina la Manase: Taanaki pamoja na malisho yake na Gati-Rimoni pamoja na malisho yake, ndio miji 2. Miji yote ilikuwa 10 pamoja na malisho yao ya kuzigawanyia koo za wana wa Kehati waliosalia. Nao wana wa Gersoni waliokuwa miongoni mwa koo za Walawi walipata kwa nusu ya shina la Manase mji wa Golani huko Basani uliokuwa wa kukimbilia wauaji pamoja na malisho yake na Bestera pamoja na malisho yake, ndio miji 2. Tena kwa shina la Isakari Kisioni pamoja na malisho yake na Daberati pamoja na malisho yake, Yarmuti pamoja na malisho yake na Eni-Ganimu pamoja na malisho yake, ndio miji 4. Tena kwa shina la Aseri: Misali pamoja na malisho yake na Abudoni pamoja na malisho yake, Helkati pamoja na malisho yake na Rehobu pamoja na malisho yake, ndio miji 4. Tena kwa shina la Nafutali: mji wa Kedesi uliokuwa wa kukimbilia wauaji kule Galili pamoja na malisho yake na Hamoti-Dori pamoja na malisho yake na Kartani pamoja na malisho yake, ndio miji 3. Miji yote, Wagersoni waliyozipatia koo zao, ilikuwa miji 13 pamoja na malisho yao. Nazo koo za wana wa Merari, ndio Walawi waliosalia, walipata kwa shina la Zebuluni: Yokinamu pamoja na malisho yake, Karta pamoja na malisho yake, Dimuna pamoja na malisho yake, Nahalali pamoja na malisho yake, ndio miji 4. Tena kwa shina la Rubeni: Beseri pamoja na malisho yake na Yasa pamoja na malisho yake. Kedemoti pamoja na malisho yake na Mefati pamoja na malisho yake, ndio miji 4. Tena kwa shina la Gadi: mji wa Rama wa Gileadi, uliokuwa wa kukimbilia wauaji, pamoja na malisho yake na Mahanaimu pamoja na malisho yake, Hesiboni pamoja na malisho yake, Yazeri pamoja na malisho yake, yote ndio miji 4. Miji yote, wana wa Merari waliosalia miongoni mwa koo za Walawi waliyozipatia koo zao kwa kupigiwa kura, ilikuwa miji 12. Miji yote ya Walawi iliyokuwa katikati ya nchi zao wana wa Isiraeli ilikuwa miji 48 pamoja na malisho yao yaliyoizunguka; miji hii ilikuwa mji kwa mji pamoja na malisho; ndivyo, miji hiyo yote ilivyokuwa. Ndivyo, Bwana alivyowapa Waisiraeli nchi hii yote, aliyoapa kuwapa baba zao, wakaichukua, wakakaa humo. Naye Bwana akawapatia utulivu pande zote pia, kama alivyowaapia baba zao, mtu asiweze kusimama mbele yao miongoni mwa adui zao wote, kwani adui zao wote Bwana aliwatia mikononi mwao. Yale mema yote, Bwana aliyowaagia wao wa mlango wa Isiraeli, halikuwapotelea hata moja, yalikuwa yametimia yote pia. Ndipo, Yosua alipowaita Warubeni na Wagadi nao waliokuwa nusu ya shina la Manase, akawaambia: Mmeyaangalia yote, Mose, mtumishi wa Bwana, aliyowaagiza, mkaisikia sauti yangu na kuyatii yote, niliyowaagiza ninyi. Hamkuwaacha ndugu zenu siku hizi nyingi mpaka siku hii ya leo, mkaliangalia agizo la Bwana Mungu wenu lililowapasa kuliangalia. Sasa Bwana Mungu wenu amewapatia ndugu zenu kutulia, kama alivyowaambia; kwa hiyo geukeni, mwende zenu mahemani kwenu katika nchi hiyo, mliyoichukua, iwe yenu, Mose, mtumishi wa Bwana, aliyowapa ng'ambo ya huko ya Yordani! Mjiangalie tu kabisa, myafanye maagizo na Maonyo, Mose, mtumishi wa Bwana, aliyowaagiza ninyi! Ni yale ya kumpenda Bwana Mungu wenu, mkiendelea katika njia zake zote, mkiyaangalia maagizo yake na kugandamana naye, tena mkimtumikia kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote. Kisha Yosua akawabariki, akawapa ruhusa kwenda zao, nao wakashika njia kwenda mahemani kwao. Nusu ya shina la Manase Mose aliwapa kukaa huko Basani, nayo nusu ya pili Yosua aliwapa kukaa na ndugu zao ng'ambo ya huku ya Yordani inayoelekea baharini; hawa nao Yosua aliwabariki alipowapa ruhusa kwenda mahemani kwao, akiwaambia kwamba: Rudini mahemani kwenu na kuyachukua mapato yenu mengi, mbuzi na kondoo wengi sana na fedha na dhahabu na shaba na vyuma na nguo nyingi mno. Hayo mliyoyateka kwa adui zenu yagawanyeni na ndugu zenu! Kisha Warubeni na Wagadi nao wale wa nusu ya shina la Manase wakarudi na kutoka kwao wana wa Isiraeli kule Silo ulioko katika nchi ya Kanaani, wakashika njia ya kwenda katika nchi ya Gileadi, ndiyo nchi, waliyoichukua, iwe yao, watue huko kwa kuagizwa na Bwana kinywani mwa Mose. Walipofika katika majimbo ya Yordani yaliyoko katika nchi ya Kanaani, wana wa Rubeni na wana wa Gadi nao wale wa nusu ya shina la Manase wakajenga huko Yordani pakubwa pa kutambikia palipoonekana hata mbali. Wana wa Isiraeli waliposikia kwamba: Tazameni, wana wa Rubeni na wana wa Gadi nao wale wa nusu ya shina la Manese wamejenga pa kutambikia upande wa kwao wa kuielekea nchi ya Kanaani katika majimbo ya Yordani ng'ambo ya huko, wana wa Isiraeli wapaone, basi, wana wa Isiraeli walipoyasikia wakakusanyika mkutano wote wa wana wa Isiraeli huko Silo, wawapandie kupiga vita. Lakini kwanza wana wa Isiraeli wakatuma wajumbe kwa wana wa Rubeni na kwa wana wa Gadi na kwa wale wa nusu ya shina la Manese katika nchi ya Gileadi; waliotumwa ni Pinehasi, mwana wa mtambikaji Elazari, na wakuu kumi wa kwenda naye, mkuu mmoja mmoja wa milango yenye baba ya mashina yote ya Waisiraeli; nao hao wakuu kila mmoja wao alikuwa kichwa cha mlango wa baba zao miongoni mwa maelfu ya Waisiraeli. Walipofika kwa wana wa Rubeni na kwa wana wa Gadi nako kwao wa nusu ya shina la Manase katika nchi ya Gileadi wakasema nao kwamba: Hivi ndivyo, wao wa mkutano wote wa Bwana wanavyosema: Huku kuyavunja maagano, mnayomvunjia Mungu wa Isiraeli, maana yake nini? Mbona sasa mmerudi nyuma na kumwacha Bwana kwa kujijengea pa kutambikia? Basi, hivyo hamkumkataa sasa Mungu mkiacha kumtii? Manza, tulizozikora kwa ajili ya Peori, hazikututoshea? Nasi hata siku hii ya leo hatujajieua kwa ajili yao, ingawa mkutano wa Bwana ulipigwa naye. Nanyi leo hivi mnarudi nyuma na kumwacha Bwana. Kweli ninyi leo hivi mnamkataa Bwana, msimtii, naye kesho ataukasirikia mkutano wote wa Waisiraeli. Nchi hii, mliyoichukua, iwe yenu, kama mnaiona kuwa chafu, haya! Itokeni kwenda katika nchi iliyo yake Bwana, Kao lake Bwana linakokaa, mjipatie katikati yetu nchi ya kuwa yenu! Lakini msimkatae Bwana mkiacha kumtii, wala sisi msitukatae mkiacha kututii mkijijengea pa kutambikia pasipokuwa pake Bwana Mungu wetu pa kutambikia. Akani, mwana wa Zera, alipouvunja ule mwiko wa kuchukua nyara, makali hayakuutokea mkutano wote wa Waisiraeli? Naye yeye hakuangamia peke yake tu kwa ajili ya hizo manza, alizozikora. Ndipo, wana wa Rubeni nao wana wa Gadi nao wale wa nusu ya shina la Manase walipowajibu na kuwaambia wale wakuu wa maelfu ya Waisiraeli: Mungu Mwenyezi ni Bwana, kweli Mungu Mwenyezi ni Bwana. Yeye anavijua, lakini Waisiraeli nao na wavijue! Kama tumemkataa Bwana kwa kuacha kumtii au kama tumemvunjia maagano, basi, Bwana, usitupatie wokovu siku hii ya leo! Kama tumejijengea pale pa kutambikia, tupate kurudi nyuma na kumwacha Bwana, au kwa kwamba tupate pa kutolea ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima pamoja na vipaji vya tambiko au pa kuchinjia ng'ombe za shukrani, basi, Bwana mwenyewe na atupatilize! Lakini hivi sivyo, ila tumevifanya hivi kwa kulihangaikia jambo hili la kwamba: Kesho wana wenu watawaambia wana wetu kwamba: Ninyi mko na bia gani na Bwana Mungu wa Isiraeli? Bwana aliuweka Yordani kuwa mpaka wa kututenga sisi nanyi, wana wa Rubeni na wana wa Gadi, hakuna fungu lenu lililoko kwa Bwana! Hivyo wana wenu wangewakomesha wana wetu, wasimwogope Bwana. Kwa hiyo twalisema: Na tujikaze kujijengea pa kutambikia! Lakini pasiwe pa kuteketezea ng'ombe nzima za tambiko wala pa kuchinjia ng'ombe zo zote za tambiko; ila pawe pa kutushuhudia sisi nanyi na vizazi vyetu vitakavyokuwa nyuma yetu, ya kama nasi tunamtumikia Bwana machoni pake na kumtolea ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na nyingine zinazoteketezwa vipande vipande tu, hata za shukrani, wana wenu wasiwaambie wana wetu kesho: Hakuna fungu lenu lililoko kwa Bwana. Kwa hiyo twalisema: Kama itakuwa, kesho watuambie sisi au vizazi vyetu maneno kama hayo, tutawaambia: Litazameni hilo jengo la mfano wa mahali pale pa kumtambikia Bwana, baba zetu walilolitengeneza, lakini hawakulitaka kuwa pa kuteketezea ng'ombe nzima za tambiko wala pa kuchinjia ng'ombe zo zote za tambiko, ila walilitaka kuwa pa kutushuhudia sisi nanyi. Na litukalie mbali shauri kama hilo la kumkataa Bwana, tusimtii, nalo la kurudi nyuma sasa na kumwacha Bwana, tukijijengea pa kutambikia, pawe pa kuteketezea ng'ombe nzima za tambiko na pa kutolea vipaji vya tambiko na pa kuchinjia ng'ombe nyingine za tambiko, pasipokuwa pale pa kumtambikia Bwana Mungu wetu palipo mbele ya Kao lake. Mtambikaji Pinehasi na wakuu wa mkutano waliokuwa vichwa vyao maelfu ya Waisiraeli waliokuwa naye walipoyasikia haya maneno, wana wa Rubeni na wana wa Gadi na wana wa Manase waliyoyasema, wakayaona kuwa mema. Ndipo, Pinehasi, mwana wa mtambikaji Elazari, alipowaambia wana wa Rubeni na wana wa Gadi na wana wa Manase: Leo hivi tunajua, ya kuwa Bwana yuko katikati yetu, kwa kuwa hamkumvunjia Bwana maagano kwa njia hiyo. Hivi ndivyo, mlivyowaokoa wana wa Isiraeli, mkono wa Bwana usiwapige. Kisha Pinehasi, mwana wa mtambikaji Elazari, akarudi pamoja na wale wakuu, wakitoka katika nchi ya Gileadi kwa wana wa Rubeni na kwa wana wa Gadi, waende katika nchi ya Kanaani kwao wana wa Isiraeli, wakawarudisha hayo majibu. Neno hili likawa jema machoni pao wana wa Isiraeli, kwa hiyo wana wa Isiraeli wakamtukuza Mungu, wasiseme tena: Na tuwapandie kupiga vita na kuiharibu hiyo nchi, wana wa Rubeni na wana wa Gadi wanakokaa. Nao wana wa Rubeni na wana wa Gadi wakapaita pale pa kutambikia Shahidi wakisema: Ndipo, panapotushuhudia, ya kuwa Bwana ni Mungu. Siku zilipopita nyingi tangu hapo, Bwana alipowapatia wana wa Isiraeli kutulia, wasipigane na adui zao wote waliowazunguka, Yosua akawa mzee kwa kuwa mwenye siku nyingi. Kwa hiyo Yosua akawaita Waisiraeli wote, wazee wao na wakuu wao na waamuzi wao na wenye amri wa kwao, kisha akawaambia: Mimi sasa ni mzee mwenye siku nyingi. Ninyi mmeyaona yote, Bwana Mungu wenu aliyowafanyizia hao wamizimu wote machoni penu, Bwana Mungu wenu akiwapigia vita. Tazameni: Nimewagawia nazo nchi zao hao wamizimu waliosalia na kuyapigia mashina yenu kura, wazipate kuwa zao toka mto wa Yordani pamoja nazo za wale wamizimu, niliokwisha kuwatowesha mpaka kwenye Bahari Kubwa, jua linakoingia. Bwana Mungu mwenyewe atawakumba, waondoke machoni penu, atawafukuza, msiwaone tena, mpate kuzichuua nchi zao, kama Bwana Mungu wenu alivyowaambia. Kwa hiyo jishupazeni sana, myaangalie na kuyafanya yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Maonyo ya Mose, msiyaache na kugeuka kuumeni wala kushotoni! Msiingie kwao hao wamizimu waliosalia kwenu, wala majina ya miungu yao msiyalilie, wala msiyakumbushe, wala msiyataje mkiapa, wala msiitumikie na kuiangukia! Ila gandamaneni na Bwana Mungu wenu, kama mlivyofanya mpaka siku hii ya leo! Naye Bwana amefukuza machoni penu mataifa makubwa yenye watu wenye nguvu, hata mmoja asiweze kusimama mbele yenu mpaka siku hii ya leo. Mtu mmoja wa kwenu hufukuza elfu wa kwao, kwani Bwana Mungu wenu ndiye anayewapigia vita, kama alivyowaambia. Kwa hiyo jiangalieni sana kwa ajili ya roho zenu, mmpende Bwana Mungu wenu! Kwani mtakaporudi nyuma na kuandamana na masao ya hao wamizimu waliosalia kwenu, mwoane nao mkiingia kwao nao wakiingia kwenu, ndipo mjue kabisa, ya kuwa Bwana Mungu wenu hataendelea kuwafukuza wamizimu hao, msiwaone tena, ila watakuwa mitego na matanzi ya kuwanasa na viboko vya kuwapiga mbavuni na miiba ya kuyachoma macho yenu, mpaka mwangamie katika nchi hii nzuri, Bwana Mungu wenu aliyowapa. Tazameni, mimi sasa ninajiendea na kuishika njia yao wote walioko huku nchini. Nanyi tambueni kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote, ya kuwa yale mema yote, Bwana Mungu wenu aliyowaagia, yamewatimilia yote pia, halikuwapotelea hata moja lao! Lakini kama yale mema yote, Bwana Mungu wenu aliyowaagia, yalivyowatimilia, vivyo hivyo Bwana atawatimizia nayo yale mabaya yote, mpaka awatoweshe katika nchi hii nzuri, Bwana Mungu wenu aliyowapa. Hayo yatafanyika, msipolishika Agano, Bwana Mungu wenu alilowaagiza, mtakapokwenda kutumikia miungu mingine na kuiangukia, basi, hapo ndipo, makali ya Bwana yatakapowawakia, mwangamie upesi na kutoweka katika nchi hii nzuri, aliyowapa ninyi. Kisha Yosua akayakusanya mashina yote ya Waisiraeli huko Sikemu, akawaita wazee wa Waisiraeli na wakuu wao na waamuzi wao na wenye amri wa kwao, wakajipanga mbele ya Mungu. Ndipo, Yosua alipowaambia watu wote: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wenu anavyosema: Tangu kale baba zenu, walipokaa ng'ambo ya huko ya lile jito kubwa, naye Tera, babake Aburahamu na babake Nahori, walitumikia miungu mingine. Ndipo, nilipomchukua baba yenu Aburahamu na kumtoa ng'ambo ya huko ya lile jito kubwa, nikamtembeza katika nchi yote ya Kanaani, nao walio wa uzao wake nikawazidisha kuwa wengi nilipokuwa nimekwisha kumpa Isaka. Naye Isaka nikampa Yakobo na Esau, naye Esau nikampa milima ya Seiri, aichukue, iwe yake, lakini Yakobo na wanawe wakashuka kwenda Misri. Kisha nikamtuma Mose na Haroni, nikaipiga nchi ya Misri kwa hayo matendo, niliyoyafanya huko kwao, kisha nikawatoa ninyi. Nilipowatoa baba zenu huko Misri, nanyi mlipofika baharini, Wamisri wakapiga mbio kuwafuata baba zenu kwa magari na kwa farasi mpaka kwenye Bahari Nyekundu. Walipomlilia Bwana, akaangusha giza jeusi, liwe katikati yenu na Wamisri; halafu akaleta bahari, iwatose na kuwafunika. Macho yenu yaliyaona hayo, niliyowafanyizia Wamisri, kisha mkakaa nyikani siku nyingi. Kisha nikawapeleka katika nchi ya Waamori wanaokaa ng'ambo ya huko ya Yordani; walipopiga vita nanyi, nikawatia mikononi mwenu, mkaichukua nchi yao, nilipowaangamiza machoni penu. Balaka, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alipoondoka kupigana na Waisiraeli, tena alipotuma kumwita Bileamu, mwana wa Beori, awaapize ninyi, sikutaka kumsikia Bileamu, naye hakuwa na budi kuwabariki ninyi, nikawaponya mkononi mwake. Kisha mkauvuka Yordani, mkafika Yeriko; tena hapo, wenyeji wa Yeriko, Waamori na Waperizi na Wakanaani na Wahiti na Wagirgasi, Wahiwi na Wayebusi, walipopigana nanyi, nikawatia mikononi mwenu, Nikatanguliza mbele yenu mavu, nao wakawafukuza mbele yenu wale wafalme wawili wa Waamori, msichomoe upanga, wala msitumie upindi. Nikawapa ninyi nchi, msiyoisumbukia, nayo miji, msiyoijenga, mkakaa humo, mkapata kula mazao ya mizabibu na ya michekele, msiyoipanda. Sasa mwogopeni Bwana na kumtumikia kwa mioyo yote na kwa welekevu, mkiiacha miungu, baba zenu waliyoitumikia ng'ambo ya huko ya lile jito kubwa nako kule Misri, mpate kumtumikia Bwana. lakini kama ni vibaya machoni penu kumtumikia Bwana, basi, jichagulieni siku hii ya leo, mtakayemtumikia, kama ni miungu, baba zenu waliyoitumikia ng'ambo ya huko ya lile jito kubwa, au kama ni miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi nao waliomo nyumbani mwangu tutamtumikia Bwana. Ndipo, watu walipojibu wakisema: Shauri hili na litukalie mbali la kumwacha Bwana na kutumikia miungu mingine. Kwani Bwana ni Mungu wetu. Yeye ndiye aliyetuleta huku na kututoa sisi na baba zetu katika nchi ya Misri nyumbani, tulimokuwa watumwa, naye ndiye aliyevifanya vile vielekezo vikubwa machoni petu, naye alituangalia katika njia zote, tulizokwenda, na katika makabila yote, ambao tulipita katika nchi zao. Yeye Bwana ndiye aliyeyafukuza makabila yote machoni petu, nao Waamori waliokuwa wenyeji wa nchi hii; kwa hiyo nasi tutamtumikia Bwana, kwani yeye ni Mungu wetu. Naye Yosua akawaambia watu: Hamwezi kumtumikia Bwana, kwani yeye ni Mungu mtakatifu, tena Mungu mwenye wivu, kwa hiyo hatayavumilia mapotovu yenu na makosa yenu. Kwani mtakapomwacha Bwana na kutumikia miungu migeni, atawafanyizia mabaya tena, awamalize ninyi akiacha kuwafanyizia mema. Lakini watu wakamwambia Yosua: Hivi havitakuwa, kwani tutamtumikia Bwana. Ndipo, Yosua alipowaambia watu: Ninyi mnajishuhudia wenyewe, ya kuwa mmejichagulia kumtumikia Bwana; nao wakaitikia kwamba: Tunajishuhudia hivyo. Naye akasema: Sasa iondoeni miungu hiyo migeni iliyoko kwenu! Kisha ielekezeni mioyo yenu kumtazamia Bwana Mungu wa Isiraeli! Ndipo, watu walipomwambia Yosua: Bwana Mungu wetu ndiye, tutakayemtumikia na kuisikia sauti yake. Ndivyo, Yosua alivyoagana na watu siku hiyo akiwatolea maongozi na maamuzi huko Sikemu. Kisha Yosua akayaandika haya mambo yote katika kitabu cha Maonyo ya Mungu, akachukua jiwe kubwa, akalisimika chini ya mkwaju uliokuwako huko kwenye Patakatifu pa Bwana. Kisha Yosua akawaambia watu wote: Tazameni! Jiwe hili na lituwie shahidi! Kwani limeyasikia maaneno yote, Bwana aliyoyasema na sisi. Kwa hiyo litakuwa shahidi lenu, msimwongopee Mungu wenu! Kisha Yosua akawapa watu ruhusa kwenda kwao kila mtu kwenye fungu lake. Ikawa, hayo yalipomalizika, akafa Yosua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, mwenye miaka 110. Wakamzika katika mipaka ya fungu lake huko Timunati-Sera ulioko mlimani kwa Efuraimu upande wa kaskazini wa mlima wa Gasi. Nao Waisiraeli wakamtumikia Bwana siku zote, Yosua alizokuwapo, nazo siku zote, walizokuwapo wale wazee waliokaa siku nyingi kuliko Yosua, ndio wale walioyajua yale matendo yote, Bwana aliyowatendea Waisiraeli. Nayo mifupa ya Yosefu, wana wa Isiraeli waliyokuja nayo walipotoka Misri, wakaizika Sikemu katika fungu lile la shamba, Yakobo alilolinunua kwa vipande mia vya fedha kwa wana wa Hamori, babake Sikemu; kwa hiyo hilo fungu likawa lao wana wa Yosefu. Elazari, mwana wa Haroni, alipokufa, wakamzika huko Gibea uliokuwa mji wa mwanawe Pinehasi, maana ndio, aliogawiwa milimani kwa Efuraimu. Yosua alipokwisha kufa, wana wa Isiraeli wakamwuliza Bwana kwamba: Yuko nani kwetu atakayeanza kupanda kwao Wakanaani kupigana nao? Bwana akasema: Yuda ndiye atakayepanda, nanyi mtaona, ya kuwa nimeitia nchi hii mikononi mwake. Ndipo, Yuda alipomwambia ndugu yake Simeoni: Panda pamoja nami katika nchi hiyo, niliyoipata kwa kura, tupigane na Wakanaani! Kisha nami nitapanda na wewe katika nchi, uliyoipata wewe kwa kura. Kwa hiyo Simeoni akaenda naye. Yuda alipopanda, Bwana akawatia Wakanaani na Waperizi mikononi mwao, wakapiga kule Bezeki watu 10000. Walipomwona Adoni-Bezeki hapo Bezeki wakapigana naye, wakawapiga Wakanaani na Waperizi. Adoni-Bezeki alipokimbia, wakamfuata upesi, wakamkamata; ndipo, walipomkata vidole gumba vya mikono na vya miguu. Naye Adoni-Bezeki akasema: Wafalme 70 waliokatwa vidole gumba vya mikono na vya miguu walikuwa wakiokota vyakula vyao chini ya meza yangu, kama nilivyofanya, ndivyo, Mungu alivyonilipisha, kisha wakampeleka Yerusalemu, akafa huko. Kisha wana wa Yuda wakapiga vita huko Yerusalemu, wakauteka, wakawapiga wenyeji kwa ukali wa panga, nao mji wakauchoma moto. Baadaye wana wa Yuda wakashuka kupigana na Wakanaani waliokaa milimani na kusini na katika nchi ya tambarare. Kisha Wayuda wakawaendea Wakanaani waliokaa Heburoni, nalo jina la Heburoni kale lilikuwa Kiriati-Arba, wakampiga Sesai na Ahimani na Talmai. Walipotoka huko wakawaendea wenyeji wa Debiri, nalo jina la Debiri kale lilikuwa Kiriati-Seferi. Hapo Kalebu akasema: Atakayepiga Kiriati-Seferi na kuuteka nitampa mtoto wangu Akisa kuwa mkewe. Otinieli, mwana na Kenazi, mdogo wake Kalebu, alipouteka, akampa mtoto wake Akisa kuwa mkewe. Ikawa, huyu alipofika kwake akamhimiza mumewe kuomba shamba kwa baba yake Kalebu: basi, Akisa aliposhuka katika punda, Kalebu akamwuliza: Unataka nini? Naye akamwambia: Nipe tunzo la kunibariki! Kwa kuwa umenipeleka katika nchi ya kusini, nipe nazo mboji za maji! Ndipo, Kalebu alipompa zile mboji zilizokuwa upande wa juu, nazo zilizokuwa upande wa chini. Nao wana wa Keni, shemeji yake Mose, walikuwa wametoka kwao Mjini kwa Mitende, wapande nao wana wa Yuda kukaa katika nyika ya Yuda iliyoko kusini kuelekea Aradi; ndivyo, walivyokuja kukaa na watu wa ukoo huo. Kisha Wayuda wakaenda pamoja na ndugu zao Wasimeoni, wakawapiga Wakanaani waliokaa Sefati, wakauangamiza wote kwa kuutia mwiko wa kuwapo, kisha wakaliita jina la mji huo Horma (Mwiko). Kisha Wayuda wakauteka Gaza na mitaa iliyoko mipakani kwake na Askaloni na mitaa iliyoko mipakani kwake na Ekroni na mitaa iliyoko mipakani kwake. Bwana akawa nao Wayuda, akawapa kuichukua milima, lakini waliokaa bondeni hawakuweza kuwafukuza, kwani walikuwa na magari ya chuma. Kisha wakampa Kalebu mji wa Heburoni, kama Mose alivyoagiza; naye akawafukuza humo wale wana watatu wa Anaki. Lakini wana wa Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa Yerusalemu, kwa hiyo Wayebusi wakakaa Yerusalemu pamoja na wana wa Benyamini mpaka siku hii ya leo. Wao wa mlango wa Yosefu walipopanda nao kuujia Beteli, Bwana akawa nao. Wao wa mlango wa Yosefu wakaupeleleza Beteli; nao jina la mji huu kale uliitwa jina lake Luzi. Walinzi walipoona mtu, akitoka mjini, wakamwambia: Tuonyeshe pa kuuingilia mji huu, nasi tutakufanyizia mambo ya upole. Alipowaonyesha pa kuuingilia mji, wakawapiga wenyeji kwa ukali wa panga, lakini yule mtu wakamwacha, ajiendee na ukoo wake wote. Naye huyo mtu akaenda katika nchi ya Wahiti, akajenga mji, akauita jina lake Luzi, ndilo jina lake mpaka siku hii ya leo. Wamanase hawakuwafukuza wenyeji wa Beti-Seani na wa mitaa yake, wala wa Taanaki na wa mitaa yake, wala wa Dori na wa mitaa yake, wala wenyeji wa Ibileamu na wa mitaa yake, wala wenyeji wa Megido na wa mitaa yake. Ndivyo, Wakanaani walivyopata kukaa kwanza katika nchi hii. Lakini Waisiraeli walipopata nguvu, wakawashurutisha Wakanaani kuwafanyia kazi za kutumwa, lakini kufukuza hawakuwafukuza. Nao Waefuraimu hawakuwafukuza Wakanaani waliokuwa wenyeji huko Gezeri, ila Wakanaani wakakaa katikati yao huko Gezeri. Nao Wazebuluni hawakuwafukuza wenyeji wa Kitironi wala wenyeji wa Nahaloli; lakini wao wakawatumikia. Nao Waaseri hawakuwafukuza wenyeji wa Ako, wala wenyeji wa Sidoni, wala wa Alabu, wala wa Akizibu, wala wa Helba, wala wa Afiki, wala wa Rehobu. Kwa hiyo Waaseri walikaa katikati ya Wakanaani waliokuwa wenyeji wa nchi hii, kwani hawakuwafukuza. Wanafutali hawakuwafukuza wenyeji wa Beti-Semesi, wala wenyeji wa Beti-Anati, wakakaa katikati ya Wakanaani waliokuwa wenyeji wa nchi hii, lakini watu wa Beti-Semesi na wa Beti-Anati wakawatumikia. Lakini Waamori wakawatesa wana wa Dani, waende milimani, wakawazuia, wasishuke kukaa bondeni. Ndivyo, Waamori walivyopata kukaa kwanza mlimani kwa Heresi na Ayaloni na Salabimu; lakini mikono yao wa mlango wa Yosefu ilipowalemea, wakawatumikia. Nayo nchi ya Waamori ilianzia hapo pa kukwelea Akarabimu, ikaendelea kutokea huko gengeni hata juu. Ndipo, malaika wa Bwana alipotoka Gilgali, akaja kupanda Bokimu, akasema: Naliwatoa Misri, nikawaleta katika nchi hii, niliyoapa kuwapa baba zenu, nikasema: Agano, nlilolifanya nanyi, sitalivunja kale na kale. Ninyi msifanye maagano na wenyeji wa nchi hii! Ila pabomoeni pao pa kutambikia! Lakini hamkuisikia sauti yangu; maana yao haya, mliyoyafanya, ndio nini? Kwa hiyo nasema nami: Sitawafukuza mbele yenu, wapate kuwasonga mbavuni, nayo miungu yao iwanase kama tanzi. Malaika wa Bwana alipowaambia wana wote wa Isiraeli maneno haya, watu wakazipaza sauti zao, wakalia. Kwa hiyo wakaliita jina la mahali hapo Bokimu (Vilio), kisha wakamtambikia Bwana. Hapo Yosua alipowapa watu wa ukoo huu ruhusa kwenda kwao, wana wa Isiraeli walikwenda kila mtu kwenye fungu lake la nchi, alichukue. Watu wakamtumikia Bwana siku zote, Yosua alizokuwapo, nazo siku zote, walizokuwapo wale wazee waliokaa siku nyingi kuliko Yosua, ndio wale walioyaona matendo makuu yote, Bwana aliyowatendea Waisiraeli. Naye Yosua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa mwenye miaka 110. Wakamzika katika mipaka ya fungu lake huko Timunati-Heresi milimani kwa Efuraimu upande wa kaskazini wa mlima wa Gasi. Watu wote wa kizazi hicho walipokwisha kukusanywa kwenda kwa baba zao, wakaondokea watu wengine wa kizazi kingine wasiomjua Bwana wala matendo, aliyowatendea Waisiraeli. Ndipo, wana wa Isiraeli walipoyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kwa kuyatumikia Mabaali. Wakamwacha Bwana Mungu wa baba zo aliyewatoa katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine miongoni mwao miungu ya makabila yaliyowazunguka, wakaiangukia. Ndivyo, walivyomkasirisha Bwana. Walipomwacha Bwana wakamtumikia Baali, nayo Maastaroti. Kwa hiyo makali ya Bwana yakawawakia waisiraeli, akawatia mikononi mwa wanyang'anyi, wawanyang'anye mali zao, namo mikononi mwa adui zao waliowazunguka, akawauza, wasiweze tena kusimama usoni pao adui zao. Po pote walipotokea, mkono wa Bwana ukawapatia mabaya, kama Bwana alivyowaambia, kama Bwana alivyowaapia; kwa hiyo wakasongeka sana. Ndipo, Bwana alipowainulia waamuzi, wawaokoe mikononi mwao waliowanyang'anya mali zao. Lakini nao waamuzi hawakuwasikia, kwani walivunja maagano kama wagoni waliofuata miungu mingine na kuiangukia; ndivyo, walivyoondoka upesi katika njia, baba zao waliyoishika, ni ile ya kuyasikia maagizo ya Bwana. Hawakuyafanya hayo. Bwana alipowainulia waamuzi, Bwana alikuwa na yule mwamuzi, awaokoe mikononi mwa adui zao siku zote za huyu mwamuzi, kwani Bwana aliwaonea uchugu, walipompigia kite kwa ajili yao waliowatesa na kuwasukumasukuma. Lakini huyo mwamuzi alipokufa, wakafanya tena mabaya kuliko baba zao wakifuata miungu mingine, waitumikie na kuiangukia; hawakuacha kabisa kuyafanya hayo matendo yao na kuishika hiyo njia yao iliyokuwa ngumu sana. Ndipo, makali ya Bwana yalipowawakia Waisiraeli, akasema: Kwa kuwa watu hawa wamelikosea Agano langu, nililowaagiza baba zao, wakikataa kuisikia sauti yangu, mimi nami sitaendelea kufukuza mbele yao watu wa hayo mataifa, Yosua aliowaacha alipokufa. Ila nitawatumia kuwajaribu Waisiraeli, kama wataiangalia njia ya Bwana, waishike, kama baba zao walivyoishika, au kama wataiacha. Kwa hiyo Bwana akayaacha hayo mataifa, wakae, asiwafukuze upesi. Kwa hiyo hakuyatia mikononi mwa Yosua. Haya ndiyo mataifa, Bwana aliyoyaacha, wakae, awatumie kuwajaribu Waisiraeli wote wasioyajua mapigano yote ya Kanaani. Huko ni kwamba tu: vizazi vingine vya wana wa Isiraeli wayajue, wapate kujifundisha mapigano, ni wale tu wasioyajua mapigano ya kale. Nayo mataifa ni haya: watawalaji watano wa Wafilisti na Wakanaani wote na Wasidoni na Wahiwi waliokaa milimani kwa Libanoni kutoka kwenye mlima wa Baali-Hermoni mpaka kufika Hamati. Hao ndio, aliowataka wa kuwajaribu Waisiraeli, ajue, kama watayasikia maagizo ya Bwana, aliyowaagiza baba zao kinywani mwa Mose. Ndivyo, wana wa Isiraeli walivyokaa katikati kwao Wakanaani na kwa Wahiti na kwa Waamori na kwa Waperizi na kwa Wahiwi na kwa Wayebusi. Wakawachukua wana wao wa kike, wawe wake zao, nao wana wao wa kike wakawapa wana wao wa kiume, nayo miungu yao wakaitumikia. Wana wa Isiraeli walipoyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, wakimsahau Bwana Mungu wao, watumikie vinyago vya Baali na vya Ashera, makali ya Bwana yakawawakia Waisiraeli, akawauza na kuwatia mkononi mwa Kusani-Risataimu, mfalme wa Mesopotamia; nao wana wa Isiraeli wakamtumikia Kusani-Risataimu miaka 8. Wana wa Isiraeli walipomlilia Bwana, Bwana akawainulia wana wa Isiraeli mwokozi, awaokoe, ndiye Otinieli, mwana wa Kenazi, mdogo wake Kalebu. Roho ya Bwana ilipomjia, akawa mwamuzi wa Waisiraeli, akatoka kwenda vitani, naye Bwana akamtia Kusani-Risataimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake, kwa kuwa mkono wake yeye ulikuwa wenye nguvu kuliko ule wa Kusani-Risataimu. Ndipo, nchi ilipopata kutulia miaka 40, kisha Otinieli, mwana wa Kenazi, akafa. Wana wa Isiraeli walipoendelea kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, Bwana akamtia Egloni, mfalme wa Moabu, nguvu, awashinde Waisiraeli, kwa kuwa waliyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana. Ndipo, alipokusanya kwake wana wa Amoni na Waamaleki, kisha akaenda, akawapiga Waisiraeli, nao Mji wa Mitende wakauchukua. Kisha Waisiraeli wakamtumikia Egloni, mfalme wa Moabu, miaka 18. Wana wa Isiraeli walipomlilia Bwana, Bwana akawainulia mwokozi, ndiye Ehudu, mwana wa Gera wa Benyamini, ni mtu mwenye shoto. Huyu wana wa Isiraeli wakamtuma kumpelekea Egloni, mflame wa Moabu, mahongo. Ehudu akajipatia upanga wenye ukali pande zote mbili, nao urefu wake kama mkono; akaufunga chini ya nguo yake penye paja lake la kuume. Akampelekea Egloni, mfalme wa Moabu, hayo mahongo, naye Egloni alikuwa mtu mnene sana. Alipokwisha kumpelekea hayo mahongo, akawapa wale watu waliochukua mahongo ruhusa kwenda zao. Lakini mwenyewe akarudia Gilgali, hapo palipokuwa na vinyago, akasema: Nina neno la njama na wewe mfalme; naye akasema: Nyamaza kwanza! Wote waliosimama kwake walipokwisha kutoka, Ehudu akaingia mwake; naye alikuwa amekaa katika chumba cha juu chenye baridi yeye peke yake tu. Ehudu aliposema: Ninalo neno la Mungu la kukuambia, akainuka katika kiti chake cha kifalme. Ndipo, Ehudu alipoupeleka mkono wake wa kushoto, akauchomoa upanga penye paja lake la kuume, akamchoma tumboni; hata kipini kikaingia ndani pamoja na chuma cha upanga, nayo mafuta yakapafungia palipoingia upanga, kwani hakuutoa upanga tumboni, nao ulitokea nyuma. Kisha Ehudu akatoka, akaja barazani, akaifunga milango ya kile chumba cha juu nyuma yake kwa komeo. Alipokwisha kutoka, watumishi wake Egloni wakaja; lakini walipoona, ya kuwa milango ya chumba cha juu imefungwa kwa makomeo, wakasema; Labda amejifunika miguu yake katika chumba cha baridi. Wakangoja kwa kuona soni, lakini walipoona ya kuwa hakuna anayeifungua milango ya chumba, wakachukua ufunguo, wakaifungua, mara wakamwona bwana wao, akilala chini, maana amekufa. Naye Ehudu alikuwa ameponyoka, wale walipokawilia, naye akapapita penye vinyago, akapona kweli alipofika Seira. Alipoingia humo akapiga baragumu milimani kwa Efuraimu; ndipo, wana wa Isiraeli waliposhuka pamoja naye kutoka milimani, naye akawaongoza. Akawaambia: Nifuateni upesi! Kwani Bwana amewatia adui zenu, hawa Wamoabu, mikononi mwenu. Ndipo, waliposhuka na kumfuata, wakavivuka vivuko vya Yordani penye njia za kwenda Moabu, kisha hawakumpa mtu ruhusa kuvuka. Wakati huo wakaua Wamoabu kama watu 10000, wote waliokuwa wanene nao wenye nguvu wote, hakuwako aliyepona. Siku hiyo Wamoabu wakanyenyekezwa kuwa chini ya mikono ya Waisiraeli; ndipo, nchi ilipopata kutulia miaka 80. Aliyemfuata ni Samugari, mwana wa Anati; akaua Wafilisti watu 600 kwa fimbo tu la kuchungia ng'ombe; hivyo yeye naye aliwaokoa Waisiraeli. Wana wa Isiraeli walipoendelea kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, Ehudu alipokwisha kufa, Bwana akawauza na kuwatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala Hasori; naye mkuu wa vikosi vyake alikuwa Sisera, naye alikaa Haroseti wa Wamizimu. Ndipo, wana wa Isiraeli walipomlilia Bwana, kwani alikuwa na magari ya chuma 900, naye aliwatesa wana wa Isiraeli kwa nguvu miaka 20. Wakati huo kulikuwako mfumbuaji wa kike, jina lake Debora, mkewe Lapidoti, naye alikuwa mwamuzi wa Waisiraeli. Huyu Debora alikaa chini ya mtende wake katikati ya Rama na Beteli milimani kwa Efuraimu, nao wana wa Isiraeli wakapanda kuja kwake kuamuliwa. Naye akatuma kumwita Baraka, mwana wa Abinoamu wa Kedesi katika nchi ya Nafutali, akamwambia: Bwana Mungu wa Isiraeli hakukuagiza: Nenda kushika njia ya kwenda mlimani kwa Tabori, uchukue kwao wana wa Nafutali nako kwao wana wa Zebuluni watu 10000 wa kwenda na wewe? Nawe utakapofika mtoni kwa Kisoni, mimi nitamtuma Sisera, mkuu wa vikosi vya Yabini, afike kwako na magari yake na mtutumo wa watu wake, nimtie mkononi mwako. Baraka akamwambia: Ukienda pamoja nami, basi, nitakwenda. lakini usipokwenda pamoja nami, sitakwenda. Akamwambia: Nitakwenda pamoja na wewe; lakini ujue: matukuzo ya njia hii, unayokwenda, hayatakuwa yako, kwani Bwana atamtia Sisera mkononi mwa mwanamke. Kisha Debora akaondoka, akaenda Kedesi pamoja na Baraka. Baraka akawaita watu wa Zebuluni na wa Nafutali kuja Kedesi. Alipopata watu 10000 kwenda naye kwa miguu yao, Debora akaenda naye kupanda huko. Lakini Mkeni Heberi alikuwa amejitenga na Wakeni wenzake, wale wana wa Hobabu, shemeji yake Mose, akalipiga hema lake kwenye mvule wa Sananimu karibu ya Kedesi. Watu walipompasha Sisera habari, ya kuwa Baraka, mwana wa Abinoamu, ameupanda mlima wa Tabori, Sisera akaagiza, magari yake yote ya chuma 900 yakusanywe, nao watu wake wote watoke Haroseti wa Wamizimu, waje mtoni kwa Kisoni. Ndipo, Debora alipomwambia Baraka: Inuka! Kwani hii ndiyo siku, Bwana atakayomtia Sisera mkononi mwako! Je? Bwana hakutoka mwenyewe kukuongoza? Kisha Baraka akashuka mlimani kwa Tabori, nao watu wake 10000 wakamfuata. Bwana akamstusha Sisera, akiyavuruga magari yote na majeshi yote kwa ukali wa panga machoni pake Baraka; ndipo, Sisera aliposhuka garini mwake, akimbie kwa miguu. Naye Baraka akayafuata mbiombio magari na majeshi mpaka Haroseti wa Wamizimu; ndiko, hayo majeshi yote ya Sisera walikopigwa kwa ukali wa panga, hakusalia hata mmoja. Naye Sisera alipokimbia kwa miguu yake akalikimbilia hema la Yaeli, mkewe Heberi, yule Mkeni, kwani Yabini, mfalme wa Hasori, na mlango wa Mkeni Heberi walikuwa wanapatana. Yaeli akatoka kumwendea Sisera njiani, akamwambia: Njoo, bwana wangu! Jiingilie mwangu, usiogope! Ndipo, alipoingia hemani mwake, naye akamfunika kwa blanketi. Kisha akamwambia: Nipe maji kidogo, ninywe! Kwani nina kiu. Akafungua kiriba cha maziwa, akamnywesha, kisha akamfunika tena. Akamwambia: Simama langoni mwa hema! Kama mtu anakuja kukuuliza kwamba: Yumo mtu? mwambie: Hapana! Kisha Yaeli, mkewe Heberi, akachukua uwambo mmoja wa hema, akatwaa nayo nyundo mkononi mwake, akamjia polepole, akaupigilia ule uwambo pajini kichwani, mpaka uingie mchangani, maana alikuwa amelala usingizi kabisa; ndipo, alipozimia, akafa. Mara akatokea Baraka aliyemfuata Sisera mbiombio, naye Yaeli akatoka kumwendea njiani, akamwambia: Njoo, nikuonyeshe yule mtu, unayemtafuta! Alipoingia mwake akamwona Sisera, akilala chini hivyo, alivyokufa, nao uwambo umo pajini. Siku hiyo ndipo, Mungu alipomnyenyekeza Yabini, mfalme wa Kanaani, machoni pao wana wa Isiraeli; nayo mikono yao wana wa Isiraeli ikazidi kumlemea Yabini, mfalme wa Kanaani, mpaka wakimwangamiza kabisa huyo Yabini, mfalme wa Kanaani. Siku ile Debora na Baraka, mwana wa Abinoamu, wakaimba kwamba: Kwa kuwa walikuwako waliowaongoza Waisiraeli, kwa kuwa nao watu wamejitoa wenyewe, kwa hiyo mtukuzeni aliye Bwana! Sikieni, ninyi wafalme! Sikilizeni, ninyi watawalaji! Mimi, mimi mwenyewe na nimwimbie Bwana, na nimshangilie Bwana Mungu wa Isiraeli! Bwana, ulipotoka Seiri, ulipopita mashambani kwa Edomu, nchi ikatetemeka, mbingu nazo zikanyesha, mawingu nayo yakanyesha mvua. Milima ikatukutika mbele ya Bwana, nao Sinai mbele yake Bwana, Mungu wa Isiraeli alipotokea. Siku za Samugari, mwana wa Anati, barabara zilikuwa zimekufa, hata siku za Yaeli; nao walioshika njia hupitia zile za kupotokapotoka. Kwao Waisiraeli hakukuwa na wakulima, walikuwa wamekoma, walikuwa wamekoma kweli, mpaka wewe, Debora, ulipotokea, nawe ukawatokea Waisiraeli kuwa mama yao. Walikuwa wamejichagulia miungu mipya; lakini vita vilipofika malangoni, haikuwako ngao wala mkuki kwao waume wa Waisiraeli, nao walikuwa maelfu arobaini. Moyo wangu huwaelekea waongozi wa Waisiraeli waliojitoa wenyewe miongoni mwa watu. Mtukuzeni aliye Bwana! Ninyi mpandao punda weupe, nanyi mkaliao mazulia, nanyi mtembeao njiani: yafikirini mioyoni! Wapiga mishale wanapocheza pamoja nao wachota maji, ndipo wayatangaze matendo ya Bwana yaongokayo, hayo matendo yaongokayo ndiyo, aliyowatendea wao waliokuwa wakulima kwao Waisiraeli. Ndipo, watu wa Bwana waliposhuka kufika malangoni. Amka! Amka, Debora! Amka! Amka, uimbe wimbo! Inuka, Baraka, upate kuwateka wanaotaka kukuteka, mwana wa Abinoamu! Ndipo, waliosalia waliposhuka kuwaendea wale watukufu, Bwana naye akashuka kuja kwangu nao hao mafundi wa vita: Efuraimu ndiko, walikotoka waliozaliwa Amaleki, Wabenyamini nao wakakufuata pamoja na watu wako wengi, kwao Wamakiri wakatoka wajuao kuongoza watu, kwao Wazebuluni wakatoka wao walioshika bakora, nazo zilikuwa zao waandaliaji wa vita. Wakuu wa Isakari wakawa naye Debora, tena kama Isakari vilevile naye Baraka, ndiye aliyejihimiza kwa miguu yake kumkimbilia pale bondeni. Lakini kule kwa vijito vya Rubeni kulikuwa na mambo, ndiyo mashauri ya mioyo yaliyo makuu. Mbona unataka kukaa tu mazizini kwa kondoo? Unataka kusikiliza mazomari yanayopigiwa makundi? Kweli vijitoni kwa Rubeni yako mashauri makuu ya mioyoni! Wagileadi wakasalia ng'ambo ya Yordani, mbona Wadani nao hukaa ugenini kwenye merikebu? Waaseri nao hukaa tu pwani kwenye bahari, kweli huwa kimya katika bandari zao. Lakini Wazebuluni ni watu wasiojiangalia kufani, Wanafutali nao ndivyo, walivyo kwao mashambani vilimani. Wafalme wakaja kufika huku, wapige vita; wafalme wa Kanaani ndio waliovipiga kule Taanaki kwenye maji ya Megido, lakini nyara, ijapo ziwe za fedha kidogo tu, hawakuzipata kabisa. Toka mbinguni wametupigania, nyota zilipokuja, zikaziacha njia zao kwa kupigana na Sisera. Kijito cha Kisoni kikawaporomosha, hicho kijito cha Kisoni kilicho kijito cha kale; roho yangu nawe, wakanyage kwa nguvu! Ndipo, zilipopiga shindo kwa kukimbia kwato za farasi, wanguvu waliowapanda walipowakimbiza. Ndivyo, asemavyo malaika wa Bwana: Uapizeni Merozi! Waapizeni! Waapizeni wao wenyeji wake! Kwani hawakufika kusaidiana na Bwana, hawakusaidiana na Bwana kwao walio mafundi wa vita. Yaeli ndiye atakayetukuzwa kuliko wenzake, mkewe Mkeni Heberi ndiye, watakayemsema mahemani, apate kutukuzwa zaidi kuliko wenzake. Alipomwomba maji, akampa maziwa, akampelekea mafuta ya maziwa katika chombo kitukufu. Akaukunjua mkono wake kuchukua uwambo, nao mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya wahunzi, akakivunja kichwa chake Sisera na kukipiga nyundo, akakiponda na kulitoboa paji lake. Miguuni pake akaanguka magotini, kisha akalala, kweli akaanguka magotini miguuni pake; alipopiga magoti, ndipo, alipoanguka, akawa mfu. Anachungulia dirishani na kulia kwa sauti kuu, mamake Sisera anachungulia katika vyuma vya dirisha: Mbona gari lake limechelewa kuja? Mbona magurudumu ya magari yake yanakawia hivyo? Wenzake wakuu wa kike wakamjibu, nao ni werevu wa kweli, naye mwenyewe akajijibu maneno yaleyale ya kwamba: Labda wameona nyara za kujigawanyia: mwanamwali mmojammoja au wawiliwawili wa kila mtu mmoja, tena ziko nguo za rangi, ndizo nyara zake Sisera, hizo nyara ni nguo za rangi zilizofumwa vizuri, ni nguo za rangi za mbalimbali, ni zenye darizi pande mbili za kupatana na shingo zao walio wenye hizo nyara. Hivyo na waangamie wote walio adui zako, Bwana! Lakini wao wampendao na wawe kama jua lenyewe, likija kucha lenye utukufu wake! Kisha nchi ikapata kutulia miaka 40. Wana wa Isiraeli walipoyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, Bwana akawatia mikononi mwao Wamidiani miaka saba. Mikono ya Wamidiani ilipowalemea Waisiraeli, wana wa Isiraeli wakajitengenezea kwa ajili ya Wamidiani mashimo yaliyokuwa milimani na mapango na magenge. Ikawa, Waisiraeli walipopanda mbegu, Wamidiani na Waamaleki na wengine waliokaa upande wa maawioni kwa jua wakapanda kwao, wakapiga makambi kwao, wakayaharibu yote yaliyozaliwa mashambani, mpaka kufika Gaza, hawakusaza kwao Waisiraeli hata nyama mmoja, wala kondoo, wala ng'ombe, wala punda. Kwani walipopanda wakaleta makundi na mahema yao, wakaja wengi mno kama nzige, hawakuhesabika wala wenyewe, wala ngamia wao, nao wakajia tu kuiharibu nchi. Waisiraeli walipopondeka sana kwa ajili ya Wamidiani, wakamlilia Bwana. Ikawa, wana wa Isiraeli walipomlilia Bwana kwa ajili ya Wamidiani, ndipo, Bwana alipotuma mfumbuaji kwa wana wa Isiraeli: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli, akawaambia: Mimi nimewaleta huku na kuwatoa Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa. Nikawaponya mikononi mwa Wamisri namo mikononi mwao wote waliowatesa, nikiwafukuza mbele yenu, kisha nikawapa nchi yao, nikawaambia: Mimi Bwana ni Mungu wenu, msiiche miungu yao Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao! Lakini hamkuisikia sauti yangu. Kisha malaika wa Bwana akaja, akakaa chini ya mkwaju kule Ofura uliokuwa wa Yoasi wa Abiezeri, mwanawe Gideoni alipokuwa akipura ngano penye kukamulia mvinyo, azifiche machoni pa Wamidiani. Malaika wa Bwana alipomtokea akamwambia: Bwana yuko pamoja na wewe uliye fundi wa vita mwenye nguvu! Gideoni akamwambia: E bwana wangu, kama Bwana yuko nasi, haya yote yamewezaje kutupata? Yako wapi matendo yake yote ya kustaajabu, baba zetu waliyotusimulia kwamba: Kumbe Bwana hakutuleta huku na kututoa Misri? Lakini sasa Bwana ametutupa, akatutia mikononi mwa Wamidiani. Ndipo, Bwana alipomgeukia na kusema: Nenda kwa hizi nguvu zako kuwaokoa Waisiraeli mikononi mwa Wamidiani! Je? Si mimi ninayekutuma? Akamwambia: E bwana wangu, niwaokoe Waisiraeli kwa nini? Tazama, udugu wetu ni mnyonge kuliko zote za Manase, nami ni mdogo nyumbani mwa baba yangu. Bwana akamwambia: Mimi nikiwa na wewe, ndipo, utakapowapiga Wamidiani, kama ni mtu mmoja tu. Naye akamwambia: Kama nimeona upendeleo machoni pako, nipatie kielekezo, nijue, ya kuwa ndiwe wewe unayesema na mimi. Usiondoke hapa, mpaka niingie nyumbani, nikuletee kipaji changu, nikiweke mbele yako. Akasema: Basi, mimi nitakaa, mpaka urudi. Ndipo, Gideoni alipoingia nyumbani, akatengeneza kidume cha mbuzi na vikate, mara moto ukatoka mwambani, ukazila hizo nyama na hivyo vikate visivyochachwa vya pishi ya unga; kisha nyama akazitia katika kikapu nao mchuzi katika nyungu, akampelekea huko chini ya mkwaju, akamkaribisha. Naye malaika wa Mungu akamwambia: Chukua hizi nyama na hivi vikate, uviweke mwambani pale, kisha vimwagie huu mchuzi. Akafanya hivyo. Naye malaika wa Bwana akaipeleka ncha ya mkongojo, aliokuwa nao mkononi, akazigusa hizo nyama na hivyo vikate. Kisha malaika wa Bwana akatoweka machoni pake. Ndipo, Gideoni alipoona, ya kuwa yeye alikuwa malaika wa Bwana; kwa hiyo Gideoni akasema: Limenipata, Bwana Mungu! Kwa kuwa nimemwona malaika wa Bwana uso kwa uso! Ndipo, Bwana alipomwambia: Tengemana tu! Usiogope! Hutakufa. Kwa hiyo Gideon akamjengea Bwana huko pa kumtambikia, akapaita Utengemano wa Bwana, napo pangalipo hata siku hii ya leo huko Ofura kwao wa Abiezeri. Ikawa usiku ule, ndipo, Bwana alipomwambia: Chukua dume la ng'ombe la baba yako na dume jingine la ng'ombe la miaka saba! Kisha pabomoe mahali pa baba yako pa kumtambikia Baali, nacho kinyago cha Ashera kilichopo hapohapo kando yake kikatekate! Kisha umjengee Bwana Mungu wako pa kumtambikia hapa juu ngomeni na kupatengeneza vema! Kisha lichukue lile dume la ng'ombe la pili, ulitoe kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ukivitumia vile vipande vya kinyago cha Ashera, ulichokikatakata, kuwa kuni! Ndipo, Gideoni alipochukua watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya, kama Bwana alivyomwagiza; lakini kwa kuwaogopa wao wa mlango wa baba yake na watu wa mjini hakuvifanya machana, ila usiku. Watu wa mjini walipoamka asubuhi na mapema, wakaona: Pa kumtambikia Baali pamebomolewa, nacho kinyago cha Ashera kilichokuwa kando yake kimekatwakatwa, nalo dume la pili limekwisha kuteketezwa lote zima hapo pengine pa kutambikia palipojengwa. Wakaulizana kila mtu na mwenzake: Ni nani aliyelifanya jambo hili? Walipotafuta hivyo na kuchunguza mwisho wakasema: Gideoni, mwana wa Yoasi, amelifanya jambo hili. Ndipo, watu wa mjini walipomwambia Yoasi: Mtoe mwanao, auawe! Kwani pa kumtambikia Baali amepabomoa, nacho kinyago cha Ashera kilichokuwa kando yake amekikatakata. Lakini Yoasi akawaambia hao wote waliosimama mbele yake: Je? Ninyi mwataka kumgombea Baali, mmwokoe? Ndiye atakayemgombea atauawa na mapema haya. Kama yeye ni mungu, na ajigombee mwenyewe, kwa kuwa wako waliopabomoa pake pa kumtambikia. Kwa hiyo watu wakamwita Gideoni siku hiyo Yerubaali, ni kwamba: Baali na ajigombee, kwa kuwa wako waliopabomoa pake pa kumtambikia. Wamidiani na Waamaleki na wengine waliokaa upande wa maawioni kwa jua walipokusanyika wote pamoja, wakavuka, wakaja kupiga makambi bondeni kwa Izireeli. Ndipo, roho ya Bwana ilipomjaa Gideoni; alipopiga baragumu, wa Abiezeri wakaitikia na kumfuata. Kisha akatuma wajumbe katika nchi yote ya Manase, nao wakaitikia na kumfuata. Hata katika nchi za Aseri na za Zebuluni na za Nafutali akatuma wajumbe, nao wakapanda kuja kuwakuta. Naye Gideoni akamwambia Mungu: Ikiwa, unataka kuwaokoa Waisiraeli kwa kuitumia mikono yangu, kama ulivyosema, basi, niweke ngozi ya kondoo yenye manyoya hapa penye kupuria ngano; kama umande utakuwa ngozini tu, nchi yote ikiwa kavu, ndipo, nitakapojua, ya kuwa utawaokoa Waisiraeli kwa kuitumia mikono yangu, kama ulivyosema. Ikawa hivyo; kesho yake alipoamka na mapema, akaikamua ile ngozi, auondoe umande humo ngozini, nayo maji yake yakajaza bakuli. Gideoni akamwambia Mungu: Makali yako yasiniwakie, nikisema tena mara hii tu kwa kuijaribu ngozi hii tena mara moja tu: ngozi pekee yake iwe kavu, lakini nchi yote ipate umande! Mungu akafanya hivyo usiku huo, ngozi ikawa kavu peke yake, lakini nchi yote ikawa yenye umande. Kisha Yerubaali, ndiye Gideoni, na watu wote waliokuwa naye, wakaondoka asubuhi, wakapiga makambi kwenye chemchemi ya Harodi, nayo makambi ya Wamidiani yalikuwa upande wa kaskazini humo bondeni nyuma ya kilima cha More. Ndipo, Bwana alipomwambia Gideoni: Watu walio kwako ni wengi, sitawatia Wamidiani mikononi mwao, Waisiraeli wasijitukuze kuliko mimi kwamba: Mikono yetu ndiyo iliyotuokoa. Sasa tangaza masikioni mwa watu kwamba: Aogopaye kwa kuwa mwenye moyo mdogo na arudi na kuondoka kilimani kwa Gileadi! Ndipo, waliporudi watu 22000, wakasalia 10000. Lakini Bwana akamwambia Gideoni: Watu wangaliko wengi bado; watelemshe kufika penye maji, ndipo, nitakapokuchagulia watu. Kila nitakayekuambia: Huyu na aende na wewe, basi, ndiye atakayekwenda na wewe; lakini kila nitakayekuambia: Huyu asiende na wewe, basi, yeye hatakwenda. Ndipo, alipowatelemsha watu kufika penye maji, naye Bwana akamwambia Gideoni: Kila atakayelamba maji kwa ulimi wake, kama mbwa anavyolamba, umweke mahali pake! Vilevile kila atakayepiga magoti yake, apate kunywa, umweke pake! Basi, hesabu yao waliolamba maji wakiyapleeka vinywani kwa viganja ikawa watu 300; wengine wote walipiga magoti yao, wapate kunywa maji. Ndipo, Bwana alipomwambia Gideoni: Nitawatumia hawa watu 300 waliolamba maji, niwaokoe ninyi nikiwatia Wamidiani mikononi mwako; lakini wale watu wote wajiendee kila mtu mahali pake! Ndipo, walipozichukua pamba za njiani za hao watu na mabaragumu yao mikononi mwao, kisha akawapa ruhusa wale Waisiraeli wote kila mtu kwenda hemani kwake, akiwashika wale 300 tu. Lakini makambi ya Wamidiani yalikuwa mle bondeni upande wa chini yake. Usiku huo Bwana akamwambia: Inuka, ushuke kufika kwenye makambi! Kwani nimewatia mikononi mwako. Lakini kama unaogopa kushuka, shuka wewe tu na kijana wako Pura, mfike kwenye makambi. Napo, utakapoyasikia wanayosemeana, ndipo, mikono yako itakapopata nguvu, ushuke kuingia makambini. Kwa hiyo akashuka yeye na kijana wake Pura, wafike pembeni kwao wenye mata waliokuwamo mle makambini. Nao Wamidiani na Waamaleki nao wote wengine waliokaa upande wa maawioni kwa jua walikuwa wamelala humo bondeni wengi mno kama nzige, nao ngamia wao hawakuhesabika, kwani walikuwa wengi kama mchanga ulioko ufukoni kwenye bahari. Gideoni alipofika, mara akasikia, mtu alivyomsimulia mwenzake ndoto na kusema: Angalia! Nimeota ndoto, nikaona, mkate wa mofa wa mawele ulivyofingirika katika makambi ya Wamidiani, ukafika kwenye hema moja, ukalipiga, lianguke, ukalifudikiza, ya chini yaje juu; basi, hilo hema likalala hivyo pale chini. Mwenzake akamjibu akisema: Hili silo jingine lisipokuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoasi, yule mtu wa Isiraeli. Mungu amewatia Wamidiani na makambi haya yote mikononi mwake. Ikawa, Gideoni aliposikia, hiyo ndoto ilivyosimuliwa, tena ilivyofumbuliwa maana, akamwangukia Mungu, kisha akarudi makambini kwa Waisiraeli, akawaambia; Inukeni! Kwani Bwana ameyatia makambi ya Wamidiani mikononi mwenu. Kisha akawagawanya wale watu 300 kuwa vikosi vitatu, akawapa kila mtu mkononi mwake baragumu na chungu kitupu kilichomo na mienge ya moto. Akawaambia: Mtakayoyaona kwangu mtayafanya nanyi. Mtakaponiona, ya kuwa nimefika pembeni kwenye makambi, ndipo mfanye sawasawa, kama mimi nitakavyofanya! Nitakapopiga baragumu mimi pamoja nao wote walioko kwangu, ndipo, nanyi mtakapoyapiga mabaragumu pande zote pia za makambi yote na kusema: Tunaye Bwana na Gideoni! Gideoni na watu mia waliokuwa naye wakafika pembeni kwenye makambi, zamu ya usiku wa manane ilipoanza, kwani papo hapo walikuwa wameweka walinzi; mara wakapiga mabaragumu pamoja na kuvivunja vyungu, walivyovishika mikononi mwao. Ndipo, vikosi vyote vitatu vilipoyapiga mabaragumu na kuvivunja vile vyungu, wakashika mikononi mwao mwa kushoto mienge, namo mikononi mwao mwa kulia yale mabaragumu ya kupiga, wakapiga makelele kwamba: Tunao upanga wa Bwana na wa Gideoni! Lakini wakasimama tu kila mtu mahali pake pande zote za makambi. Ndipo, majeshi yote yalipopiga mbio na kulia sana, yakakimbia kabisa. Yale mabaragumu 300 yalipolia, Bwana akazielekeza panga zao wenyewe, kila mtu ampige mwenzake katika makambi yote; ndipo, hayo majeshi yalipokimbia mpaka Beti-Sita kunakoelekea Serera, wengine mpaka mto wa Abeli-Mehola karibu ya Tabati. Kisha Waisiraeli wakaitwa katika nchi za Nafutali na za Aseri na za Manase pia, wakawakimbiza Wamidiani. Gideoni akatuma wajumbe kwenda milimani po pote kwa Efuraimu kwamba: Shukeni kuwajia Wamidiani, mfike mbele yao kwenye maji ya Beti-Bara, hata kwenye Yordani. Watu wote wa Efuraimu wakaitikia, wakapapata pote palipo penye maji mpaka Beti-Bara, nao Yordani. Wakakamata wakuu wawili wa Midiani, Orebu (Kunguru) na Zebu (Chui), wakamwua Orebu penye Mwamba wa Kunguru, naye Zebu wakamwua penye Kamulio la Chui. Walipokwisha kuwafukuza Wamidiani, wakavichukua vichwa vyao Orebu na Zebu ng'ambo ya huko ya Yordani, wakampelekea Gideoni. Watu wa Efuraimu wakamwuliza: Kwa nini umetufanyizia hivi, usituite, ulipokwenda kupigana na Wamidiani? Wakamgombeza kwa nguvu. Naye akawaambia: Sasa mimi nimefanya nini, nijifananishe nanyi? Maokotezo ya Efuraimu siyo mema kuliko mavuno ya Abiezeri? Mikononi mwenu Mungu amewatia wakuu wa Wamidiani, Orebu na Zebu; nami nimeweza kufanya nini, nijifananishe nanyi? Ndipo, roho zao zilipomtulilia kwa kusema maneno haya. Gideoni alipoufikia Yordani, akauvuka yeye na wale watu 300 waliokuwa naye, lakini walikuwa wamechoka kwa kuwakimbiza adui. Kwa hiyo akawaambia watu wa Sukoti: Wapeni watu hawa wanaonifuata mikate! Kwani wamechoka, nami ninawakimbiza wafalme wa Midiani, Zeba na Salmuna. Lakini wakuu wa Sukoti wakamwambia: Je? Makonde ya Zeba na ya Salmuna yamo sasa mkononi mwako, tuwape mikate watu wa vikosi vyako? Gideoni akawaambia: Basi; hapo, Bwana atakapomtia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, ndipo, nitakapoziponda nyama za miili yenu kwa miiba ya nyikani na kwa mikunju. Alipotoka huko akapanda Penueli, nao wa huko akawaambia yaleyale, lakini watu wa Penueli wakamjibu, kama watu wa Sukoti walivyomjibu. Ndipo, alipowaambia nao watu wa Penueli kwamba: Nitakaporudi salama, nitaubomoa mnara huu. Lakini Zeba na Salmuna walikuwa huko Karkori pamoja na majeshi yao, kama watu 15000, ndio wote waliosalia wa hayo majeshi yao waliokaa upande wa maawioni kwa jua; nao waliouawa walikuwa 120000 waliojua wote kutumia panga. Gideoni akashika njia yao wanaosafiri na kukaa mahemani iliyopita Noba na Yogibeha upande wa Maawioni kwa jua, akayapiga yale majeshi, kwani majeshi hayo yalikuwa yakitulia tu. Ndipo, Zeba na Salmuna walipokimbia, lakini akawafuata mbiombio, akawakamata hawa wafalme wawili wa Midiani, Zeba na Salmuna, nayo majeshi yote akayatapanya kwa kuyastusha. Gideoni, mwana wa Yoasi, alipotoka vitani, arudi, akashika njia ya juu ipitayo Heresi. Huko akakamata kijana wa Sukoti wa kumwuliza, naye akamwandikia majina ya wakuu wa Sukoti na ya wazee na huko 77. Alipofika kwao wale watu wa Sukoti akawaambia: Watazameni akina Zeba na Salmuna, ambao mlinisimanga kwa ajili yao kwamba: Je? Makonde ya Zeba na ya Salmuna yamo sasa mkononi mwako, tuwape mikate watu wako waliochoka? Kisha akawachukua wazee wa mji na miiba ya nyikani na mikunju, akaitumia ya kuwafundisha watu wa Sukoti. Kisha akaubomoa mnara wa Penueli, nao watu wa mji huu akawaua. Kisha akamwuliza Zeba na Salmuna: Wale watu, mliowaua huko Tabori walikuwa wenye sura gani? Wakasema: Walikuwa kama wewe, kila mmoja wao; ukimtazama, alikuwa kama mwana wa mfalme. Ndipo, aliposema: Ndio ndugu zangu, wana wa mama yangu. Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, kama mngaliwaacha, wakae, nisingewaua ninyi! Kisha akamwambia Yeteri, mwanawe wa kwanza: Inuka, uwaue! Lakini huyu kijana hakuuchomoa upanga wake kwa kuwa na woga, kwani angaliko kijana. Ndipo, Zeba na Salmuna waliposema: Inuka wewe, utupige! Kwani mtu alivyo, ndivyo, nazo nguvu zake zilivyo. Ndipo, Gideoni alipoinuka, akamwua Zeba, naye Salmuna, akayachukua manyamwezi yaliyokuwa shingoni pa ngamia wao. Kisha watu wa Kiisiraeli wakamwambia Gideoni: Sharti ututawale wewe na mwanao na mjukuu wako, kwa kuwa umetuokoa mikononi mwa Wamidiani. Lakini Gideoni akawaambia: Mimi sitawatawala ninyi, wala mwanangu hatawatawala ninyi, sharti Bwana awatawale ninyi. Kisha Gideoni akawaambia: Liko moja, ninalolitaka kwenu: Nipeni kila mtu mapete ya masikioni, aliyoyateka, kwani walivaa mapete ya masikioni ya dhahabu kwa kuwa Waisimaeli. Wakasema: Tutakupa kabisa. Wakatanda nguo zao, wakatupia humo kila mtu mapete yake ya masikioni, aliyoyateka. Uzito wa haya mapete ya dhahabu ya masikioni, aliyoyataka, ukawa mzigo mkubwa wa mtu (sekeli 1700 za dhahabu, ndio ratli 62) pasipo manyamwezi na mapambo mengine ya masikioni na mavazi ya kifalme, wafalme wa Wamidiani waliyoyavaa, tena pasipo mikufu ya shingoni pa ngamia wao. Kisha Gideoni akazitumia hizo dhahabu za kutengeneza kisibau cha mtambikaji, akakiweka mjini kwake Ofura. Kwa kukitambikia huko Waisiraeli wote wakamfanyia Mungu ugoni; ndivyo, kilivyokuwa tanzi la kumnasa Gideoni na mlango wake. Wamidiani kwa hivyo, walivyonyenyekezwa mbele ya wana wa Isiraeli, hawakuviinua tena vichwa vyao, kwa hiyo nchi ikapata kutulia katika siku za Gideoni miaka 40. Kisha Yerubaali, mwana wa Yoasi, akaenda zake kukaa nyumbani kwake. Yeye Gideoni akapata wana 70, aliowazaa, kwani alikuwa na wanawake wengi. Hata suria aliyekaa Sikemu akamzalia mwana, naye akamwita jina lake Abimeleki (Baba ni Mfalme). Gideoni, mwana wa Yoasi, akafa, mwenye uzee mwema, akazikwa kaburini mwa baba yake Yoasi kule Ofura kwa Abiezeri. Gideoni alipokwisha kufa, wana wa Isiraeli wakamfanyia Mungu ugoni tena na kuyafuata Mabaali, wakamtumia Baali la agano kuwa mungu wao. Kwani wao wana wa Isiraeli hawakumkumbuka Bwana Mungu wao aliyewaponya mikononi mwa adui zao wote waliowazunguka, wala mlango wa Yerubaali, ndiye Gideoni, hawakuutedea mambo ya upole, kwamba wayalipe hayo mema yote, aliyowafanyizia Waisiraeli. Abimeleki, mwana wa Yerubaali, akaenda Sikemu kwa ndugu za mama yake, akawaambia wao nao wote walio wa ukoo wa mlango wa baba ya mama yake kwamba: Semeni masikioni mwao wote walio wenyeji wa Sikemu: Lililo jema lenu ni lipi? Watu 70 walio wote wana wa Yerubaali wawatawale, au awatawale mtu mmoja? Tena kumbukeni, ya kuwa huyu ni mwenzenu kwa mifupa na kwa nyama za mwili wake. Nao ndugu za mama yake walipoyasema maneno hayo yote kwa ajili yake masikioni mwao wenyeji wote wa Sikemu, mioyo yao ikageuka kumfuata Abimeleki, kwani walisema: Yeye ni ndugu yetu! Wakampa fedha 70, walizozitoa nyumbani mwa Baali la agano, naye Abimeleki akazitumia kujipatia watu wenye ukorofi wasiokuwa na kitu cho chote, wafuatane naye. Kisha akaenda Ofura nyumbani mwa baba yake, akawaua ndugu zake, wana wa Yerubaali, wote 70 juu ya jiwe moja, akasalia tu Yotamu, mwanawe mdogo Yerubaali, kwa kuwa alijificha. Kisha wenyeji wote wa Sikemu wakakusanyika nao wote waliokaa bomani, wakaenda, wakamfanya Abimeleki kuwa mfalme huko kwenye huo mvule wa ngomeni ulioko Sikemu. Watu walipompasha Yotamu habari hizi, akaenda, akasimama juu ya mlima wa Gerizimu, akapaza sauti yake, akawaitia kwamba: Nisikilizeni, ninyi wenyeji wa Sikemu, Mungu naye awasikie! Miti ilikwenda kupaka mmoja mafuta, awe mfalme wao, ikauambia mchekele: Ututawale wewe! Lakini mchekele ukaiambia: Niache kuzaa mafuta, nayo ndiyo, wanayoniheshimia Mungu na watu? Nitawezaje kwenda kuning'inia juu ya miti? Ndipo, miti ilipouambia mkuyu: Haya! Wewe ututawale sisi! Mkuyu nao ukaiambia: Niache kuzaa matunda yangu matamu yaliyo mazuri mno? Nitawezaje kwenda kuning'inia juu ya miti? Ndipo, miti ilipouambia mzabibu: Haya! Wewe ututawale sisi! Lakini mzabibu nao ukaiambia: Niache kuzaa mvinyo zangu mbichi zinazowafurahisha wote, Mungu na watu? Nitawezaje kwenda kuning'inia juu ya miti? Ndipo, miti yote ilipouambia mchongoma: Haya! Wewe ututawale sisi! Mchongoma ukaiambia miti: Kama mnataka kweli kunipaka mafuta, niwe mfalme wenu, njoni, mkae pasipo woga kivulini pangu! Kama hamtaki, moto na utoke katika mchongoma, uile miangati ya Libanoni. Sasa ninyi je? Mmejitokeza kuwa wenye kweli na welekevu mlipomfanya Abimeleki kuwa mfalme? Au Yerubaali nao walio wa mlango wake mmewatendea mema na kuwafanyizia, kama mikono yake ilivyowafanyizia ninyi? Kwani baba yangu aliwapigia vita na kujitoa mwenyewe, apate kuwaponya mikononi mwa Wamidiani. Lakini ninyi mmeuinukia leo mlango wa baba yangu mkiwaua wanawe 70 juu ya jiwe moja, mkamfanya Abimeleki, mwana wa kijakazi wake, kuwa mfalme wa wenyeji wa Sikemu, kwa kuwa ni ndugu yenu. Bai, kama mmejitokeza kuwa wenye kweli na welekevu katika mambo haya, mliyomfanyizia leo Yerubaali nao walio wa mlango wake, na mmfurahie Abimeleki, naye na awafurahie ninyi! Lakini kama sivyo, moto na utoke kwake Abimeleki, uwale wenyeji wa Sikemu nao wakaao bomani! Tena moto na utoke kwao wenyeji wa Sikemu nako kwao wakaao bomani, umle Abimeleki! Kisha Yotamu akapiga mbio kukimbia, akafika Beri, akakaa huko na kujificha, ndugu yake Abimeleki asimwone. Abimeleki alipowatawala Waisiraeli miaka mitatu, Mungu akatuma roho mbaya, Abimeleki na wenyeji wa Sikemu wakosane, nao wenyeji wa Sikemu wakamdanganya Abimeleki na kuyavunja maagano yao. Yakafanyika hayo kwamba makorofi, wale wana 70 wa Yerubaali waliyotendewa, yalipizwe, nazo damu zao zimjie ndugu yao Abimeleki aliyewaua, ziwajie nao wenyeji wa Sikemu walioishupaza mikono yake, apate nguvu za kuwaua ndugu zake. Kwa kumtakia mabaya wenyeji wa Sikemu wakaweka washambuliaji juu ya milima, wawanyang'anye mali zao wote waliopita njiani hapo, walipokuwa. Naye Abimeleki akapashwa habari hizi. Kisha Gali, mwana wa Ebedi, akaja na ndugu zake, akapita kuingia Sikemu, nao wenyeji wa Sikemu walikuwa wanamjetea. Walipotoka kwenda shambani kuvuna zabibu na kuzikamua, wakafanya sikukuu, wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala, wakanywa, kisha wakamwapiza Abimelei. Ndipo, Gali, mwana wa Ebedi, aliposema: Abimeleki ni nani? nasi Wasikemu tu wa nani, tumtumikie? Siye mwana wa Yerubaali? Naye Zebuli siye msimamizi wake? Watumikieni watu wa Hamori aliye baba yao Wasikemu! Kwa nini sisi tumtumikie yeye? Kama mtu angewatia watu hawa mkononi mwangu, ningemwondoa Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki: Haya! Ongeza vikosi vyako, utoke! Zebuli, mkuu wa mji, alipoyasikia haya maneno ya Gali, mwana wa Ebedi, makali yake yakawaka moto. Kwa ujanja wake akatuma wajumbe kwenda kwa Abimeleki kwamba: Tazama, Gali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Sikemu, nao hujulikana, ya kuwa wanawahimiza watu wa mji, wakukatae. Sasa ondoka usiku huu, wewe na watu wako walioko kwako, uvizie shambani! Tena asubuhi, jua litakapokucha, ujidamke, uushambulie mji huu! Hapo utakapomwona, akikutokea yeye pamoja nao wote walioko kwake, utamfanyizia, mkono wako utakayoyaona. Ndipo, Abimeleki alipoondoka usiku pamoja na watu wote waliokuwa kwake, wakauvizia Sikemu kwa vikosi vinne. Gali, mwana wa Ebedi, alipotoka na kusimama hapo pa kuliingilia lango la mji, Abimeleki akaondoka hapo, alipokuwa anavizia pamoja na wale watu waliokuwa kwake. Gali alipowaona hao watu akamwambia Zebuli: Tazama! Wako watu wanaotelemka toka milimani juu! Lakini Zebuli akamwambia: Vivuli vya milima unaviona kuwa kama watu. Naye Gali akasema tena kwamba: Tazama! Ni watu wanaotelemka kutoka katikati ya nchi hii, nacho kikosi kimoja kinatoka na kushika njia ya kwenda kenye mvule, wanakotambikia. Zebuli akamwambia: Sasa kiko wapi kinywa chako kilichosema: Abimeleki ni nani, tumtumikie? Kumbe hao watu sio, uliowabeua? Haya! Toka sasa, upigane nao! Ndipo, Gali alipotoka akiwatangulia wenyeji wa Sikemu, akapigana na Abimeleki. Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akamkimbia, wakaumizwa watu wengi, wakaanguka hapohapo mpaka pa kuingia langoni penye mji. Abimeleki akakaa Aruma, lakini Zebuli akamfukuza Gali na ndugu zake, wasikae Sikemu tena. Kesho yake watu walipokwenda shambani, naye Abimeleki alipopata habari, akawachukua watu wake, akawagawanya kuwa vikosi vitatu, akawavizia hapo shambani. Alipochungulia, mara akaona, watu wakitoka mjini, akawainukia, akawapiga. Mara Abimeleki na kikosi kilichokuwa naye wakavuka kwenda mbele, wakasimama pa kuingia langoni penye mji, navyo vikosi viwili vikawarukia wote waliokuwako mashambani, vikawaua. Abimeleki alipopigana nao wa mjini mchana kutwa, akauteka huo mji, nao watu waliokuwamo akawaua, nao mji akaubomoa kabisa, kisha akaumwagia chumvi. Wote waliokaa katika mnara wa Sikemu walipoyasikia wakajificha shimoni mle nyumbani mwa mungu wao wa agano. Abimeleki alipopata habari, ya kuwa wote waliokaa katika mnara wa Sikemu wamekusanyika, Abimeleki akaupanda mlima wa Salmoni yeye pamoja na watu wote waliokuwa kwake, naye Abimeleki akachukua shoka mkononi mwake, akakata matawi ya miti, akayachukua na kujitwika mabegani, akawaambia wale watu waliokuwa naye: Mtakayoyaona, ya kuwa nimeyafanya, yafanyeni nanyi upesi kama mimi! Kwa hiyo nao watu wote wakakata matawi wakimfuata Abimeleki, wakayaweka juu ya lile shimo, wakayachoma moto juu yao waliomo shimoni; ndivyo, walivyokufa nao watu wote waliokaa katika mnara wa Sikemu, ni kama watu 1000 wanawaume na wanawake. Kisha Abimeleki akaenda Tebesi, akapiga makambi kule Tebesi, kisha akauteka. Katikati ya mji palikuwa na mnara wenye nguvu; ndimo, walimokimbilia wanawaume na wanawake wote na wenyeji wote wa huo mji, wakafunga nyuma yao, wakapaa kipaani pa mnara. Abimeleki alipofika penye mnara huo kupiga vita huko, akaukaribia mlango wa mnara, auchome moto. Ndipo, mwanamke mmoja alipomtupia Abimeleki kichwani pake jiwe la sago, likakivunja kichwa chake. Naye akamwita upesi kijana aliyemchukulia mata yake, akamwagiza: Uchomoe upanga wako, uniue, watu wasiseme, ya kama mwanamke ameniua! Ndipo, kijana wake alipomchoma upanga, kisha akafa. Waisiraeli walipoona, ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaenda zao kila mtu mahali pake. Ndivyo, Mungu alivyoyalipiza yale mabaya ya Abimeleki, aliyomfanyizia baba yake na kuwaua ndugu zake 70. Nayo mabaya ya watu wa Sikemu Mungu aliwarudishia vichwani pao; ndivyo, kiapizo cha Yotamu, mwana wa Yerubaali, kilivyowajia. Baada ya Abimeleki akaondokea Tola, mwana wa Pua, mwana wa Dodo wa Isakari, awaokoe Waisiraeli. Naye alikuwa anakaa Samiri milimani kwa Efuraimu. Akawa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 23, kisha akafa, akazikwa Samiri. Baada yake huyu akaondokea Yairi wa Gileadi, akawa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 22. Akawa mwenye wana 30 waliopanda wana wa punda 30, nao walikuwa wenye miji 30, nayo huitwa hata siku hii ya leo Mahema ya Yairi, nayo iko katika nchi ya Gileadi. Yairi alipokufa akazikwa huko Kamoni. Wana wa Isiraeli walipoendelea kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, wakiyatumikia Mabaali na Maastaroti na miungu ya Ushami na miungu ya Sidoni na miungu ya Moabu na miungu ya wana wa Amoni na miungu ya Wafilisti, basi, walipomwacha Bwana hivyo, wasimtumikie, makali ya Bwana yakawawakia Waisiraeli, akawauza na kuwatia mikononi mwa Wafilisti namo mikononi mwa wana wa Amoni. Wakawasumbua wana wa Isiraeli na kuwakorofisha; mwaka huo ikawa miaka 18, wakiwaumiza wana wa Isiraeli wote waliokaa ng'ambo ya huko ya Yordani kule Gileadi katika nchi ya Waamori. Wana wa Amoni walipovuka Yordani kupiga vita hata katika nchi ya Yuda na ya Benyamini nako kwao wa mlango wa Efuraimu, Waisiraeli wakasongeka sana. Ndipo, wana wa Isiraeli walipomlilia Bwana kwamba: Tumekukosea, tulipomwacha Mungu wetu na kuyatumikia Mabaali. Naye Bwana akawaambia wana wa Isiraeli: Sikuwatoa kwao Wamisri na Waamori na wana wa Amoni na Wafilisti? Napo, Wasidoni na Waamaleki na Wamaoni walipowatesa ninyi, nanyi mliponililia, nikawaokoa mikononi mwao. Lakini ninyi mmeniacha, mkatumikia miungu mingine; kwa hiyo sitawaokoa tena. Haya! Nendeni kuililia miungu, mliyoichagua, hiyo na iwaokoe siku za masongano yenu! Lakini wana wa Isiraeli wakamwambia Bwana: Tumekosa! Tufanyizie yote yaliyo mema machoni pako! Lakini tuponye siku hii ya leo tu! Kisha wakaiondoa hiyo miungu migeni katikati yao, wakamtumikia Bwana; ndipo, roho yake ilipoona uchungu kwa ajili ya masumbuko yao Waisiraeli. Kisha wana wa Amoni wakaitwa kukusanyika, wakapiga makambi huko Gileadi; wana wa Isiraeli nao wakapiga makambi Misipa. Ndipo, watu na wakuu wa Gileadi waliposemeana kila mtu na mwenzake: Ni nani atakayeanza kupigana nao wana wa Amoni? Yeye atakuwa mkuu wao wote wakaao Gileadi. Kulikuwa na fundi wa vita mwenye nguvu, ndiye Yefuta wa Gileadi; naye alikuwa mwana wa mwanamke mgoni, naye Gileadi ndiye aliyemzaa Yefuta. Naye mkewe Gileadi alikuwa amemzalia wana; hao wana wa huyu mwanamke walipokua wakamfukuza Yefuta wakimwambia: Haifai, ukipata urithi nyumbani mwa baba yetu, kwani wewe u mwana wa mwanamke mwingine. Ndipo, Yefuta alipowakimbia ndugu zake, akakaa katika nchi ya Tobu, wakakusanyika kwake watu wasiokuwa na kitu cho chote, nao hutoka naye kwenda huko na huko. Siku zilipopita, wana wa Amoni wakaja kupigana na Waisiraeli. Ikawa, wana wa Amoni walipokuja kupigana na Waisiraeli, ndipo, wazee wa Gileadi walipokwenda kumchukua Yefuta katika nchi ya Tobu, wakamwambia Yefuta: Njoo, uwe kiongozi wetu, tupate kupigana na wana wa Amoni! Lakini Yefuta akawaambia wazee wa Gileadi: Je? Ninyi ham wachukivu wangu? Hamkunifukuza nyumbani mwa baba yangu? Mbona sasa mnaposongwa mwanijia mimi? Ndipo, wazee wa Gileadi walipomwambia Yefuta: Kweli ni kwa sababu hii, tukirudi kwako; sasa nenda pamoja na sisi, tupate kupigana na wana wa Amoni, nawe uwe kichwa chetu sisi sote tukaao Gileadi! Naye Yefuta akawauliza wazee wa Gileadi: Mkinirudisha kwenu, nipigane nao wana wa Amoni, naye Bwana akiwatoa, waangamie mbele yangu, mimi nitakuwa kweli kichwa chenu? Wazee wa Gileadi wakamwambia Yefuta: Bwana ndiye anayeyasikia, tunayoyasemeana; na atuhukumu, tusipoyafanya uliyoyasema. Ndipo, Yefuta alipokwenda pamoja na wazee wa Gileadi, nao watu wakamweka kuwa kichwa chao na kiongozi wao. Naye Yefuta akasema maneno yake yote kule Misipa masikioni pa Bwana. Kisha Yefuta akatuma wajumbe kwa mfalme wa wana wa Amoni kwamba: Tuko na mapitano gani mimi na wewe, ukinijia kupiga vita katika nchi yangu? Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu wajumbe wa Yefuta: Kwa kuwa Waisiraeli wameichukua nchi yangu kutoka Arnoni mpaka Yaboko na Yordani, walipotoka Misri kuja huku; sasa hizi nchi zirudishe pasipo kupiga vita! Ndipo, Yefuta alipotuma mara ya pili wajumbe kwa mfalme wa wana wa Amoni, akamwambia: Hivi ndivyo, Yefuta anavyosema: Waisiraeli hawakuchukua nchi ya Wamidiani wala nchi ya wana wa Amoni. Kwani walipotoka Misri kuja huku, Waisiraeli walishika njia ya nyikani mpaka kufika kwenye Bahari Nyekundu, wakaingia Kadesi. Ndipo, Waisiraeli walipotuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu kwamba: Na tupite katika nchi yako! Lakini mfalme wa Edomu hakuwasikia; naye mfalme wa Moabu akakataa, walipotuma kwake. Kwa hiyo Waisiraeli wakakaa kwanza Kadesi, kisha wakapita nyikani na kuizunguka nchi ya Edomu na nchi ya Moabu. Walipoifikia nchi ya Moabu upande wa maawioni kwa jua wakapiga makambi ng'ambo ya Arnoni pasipo kuingia mipakani kwa Moabu, kwani Arnoni ndio mpaka wa Moabu. Ndipo, Waisiraeli walipotuma wajumbe kwa Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyetawala Hesiboni, nao Waisiraeli wakamwambia: Na tupite katika nchi yako, tufike mahali petu! Lakini Sihoni hakuwategemea Waisiraeli, hakuacha, wapite mipakani kwake, ila Sihoni akawakusanya watu wake wote, wakapiga makambi kule Yasa. Lakini alipopigana na Waisiraeli, Bwana Mungu wa Isiraeli akamtia Sihoni pamoja na watu wake wote mikononi mwa Waisiraeli, wakawapiga. Ndipo, Waisiraeli walipoichukua nchi yote nzima ya Waamori waliokaa katika nchi hii, iwe yao. Wakaichukua nchi yote iliyokuwa mipakani kwa Waamori, iwe yao toka Arnoni mpaka Yaboko, tena toka nyikani mpaka Yordani. Bwana Mungu wa Isiraeli alipokwisha kuwafukuza Waamori mbele yao walio ukoo wake wa Waisiraeli, sasa wewe unataka kuwafukuza? Kumbe Mungu wako Kamosi anayokupa kuwa mali zako huyachukui, yawe yako? Nayo yote, Bwana Mungu wetu anayotupa machoni petu kuwa yetu, basi, sisi huyachukua. Sasa je? Wewe u mwema kuliko Balaka, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu? Aligombana nao Waisiraeli, apige vita nao? Nao Waisiraeli hawakukaa Hesiboni na katika mitaa yake, hata Aroeri na katika mitaa yake na katika miji yote iliyoko pande zote mbili za Arnoni miaka 300? Mbona wakati huo hamkutaka kuipokonya? Mimi sikukukosea wewe, lakini wewe unanifanyizia vibaya ukija kupigana na mimi. Bwana aliye mwamuzi wa kweli na atuamue leo sisi wana wa Isiraeli nanyi wana wa Amoni. Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuyasikia maneno ya Yefuta, aliyotuma kumwambia. Ndipo, roho ya Bwana ilipomjia Yefuta, akaenda kupita katika nchi ya Gileadi na ya Manase, kisha akaenda Misipe wa Gileadi, toka Misipe wa Gileadi akawaendea wana wa Amoni. Ndipo, Yefuta alipomwapia Bwana kiapo kwamba: Kama utawatia wana wa Amoni mikononi mwangu, nami nikirudi salama katika vita vya wana wa Amoni, ndipo, yule atakayetoka wa kwanza milangoni mwa nyumbani mwangu, anijie njiani, atakuwa wake Bwana, nami nitamtoa kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Kisha Yefuta akawaendea wana wa Amoni kupigana nao, naye Bwana akawatia mikononi mwake. Akawapiga kutoka Aroeri, mpaka mtu akifika Miniti kwenye miji ishirini hata Abeli-keramimu (Mbuga ya Mizabibu), pigo hilo likawa kubwa sana. Ndivyo, wana wa Amoni walivyonyenyekezwa mbele yao wana wa Isiraeli. Yefuta alipofika Misipa kwenye nyumba yake, mara mwanawe wa kike akatoka kumwendea njiani akipiga patu na kuchezacheza, naye alikuwa mwanawe wa pekee, kuliko yeye hakuwa na mwana mwingine, wala wa kiume, wala wa kike. Ikawa, alipomwona akazirarua nguo zake akilia: E mwanangu! Unaninyenyekeza sana! Kumbe wewe nawe u mmoja wao wanaonisikitisha! Mimi nimekifumbua kinywa changu kusema na Bwana, siwezi kuyarudisha niliyoyasema. Naye akamwambia: Baba yangu, kama umekifumbua kinywa chako kusema na Bwana, nifanyizie, kama kinywa chako kilivyosema! Kwa kuwa Bwana amekupa kuwalipiza adui zako, hao wana wa Amoni. Kisha akamwambia baba yake: Hili moja tu nilipate: Niache miezi miwili, niende kutembea milimani, niuombolezee uwanawali wangu, mimi pamoja na wenzangu. Akamwambia: Basi, nenda kwanza! akampa ruhusa kujiendea miezi miwili. Naye akaenda na wenzake, akauombolezea uwanawali wake huko milimani. Hiyo miezi miwili ilipokwisha, akarudi kwa baba yake, naye akamtimilizia kiapo chake, alichokiapa; naye alikuwa hajatambua mtu mume. Tangu hapo ikawa desturi kwao Waisiraeli, vijana wa kike wa Waisiraeli waende mwaka kwa mwaka kumwimbia matukuzo binti Yefuta wa Gileadi siku nne. Waefuraimu wakaitwa kukusanyika, wakaenda upande wa kaskazini, wakamwambia Yefuta: Kwa sababu gani ulikwenda kupigana nao wana wa Amoni, usituite kwenda pamoja na wewe? Sasa tutaichoma moto nyumba yako juu yako. Lakini Yefuta akawaambia: Vita, tulivyovipiga mimi na watu wangu na wana wa Amoni, vilikuwa vikali mno, nami nilipowaita ninyi, hamkuniokoa mikononi mwao. Nilipoona, ya kuwa ninyi hamniokoi, nikajitoa mwenyewe, nikawaendea wana wa Amoni, naye Bwana akawatia mikononi mwangu Ni kwa sababu gani, mkinipandia leo hivi kupigana na mimi? Kisha Yefuta akawakusanya watu wote wa Gileadi, apigane na Waefuraimu; nao watu wa Gileadi wakawapiga Waefuraimu, kwani walikuwa wamesema: Ninyi m watoro wa Efuraimu, maana Gileadi uko katikati ya nchi ya Efuraimu na ya Manase. Lakini Wagileadi walivitwaa vivuko vya Yordani vya kwenda Efuraimu. Vikawa hivyo: kila mara watoro wa Efuraimu waliposema: Na nivuke, watu wa Gileadi wakamwuliza: Wewe u Mwefuraimu? Naye aliposema: Hapana, wakamwambia: Tamka Shiboleti! Tena aliposema: Siboleti kwa kuwa hakuweza kutamka Shiboleti, wakamkamata, wakamwua hapo penye vivuko vya Yordani; ndivyo, walivyouawa wakati huo Waefuraimu 42000. Yefuta akawa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 6, kisha Yefuta wa Gileadi akafa, akazikwa katika mmoja wao miji ya nchi ya Gileadi. Baada yake Ibusani wa Beti-Lehemu akawa mwamuzi wa Waisiraeli. Alikuwa mwenye wana wa kiume 30 na wa kike 30, ndio aliowaoza kwenda pengine, tena aliingiza wanawake wengine 30 toka pengine, wawe wake za wanawe. Akawa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 7. Ibusani alipokufa akazikwa Beti-Lehemu. Baada yake Eloni wa Zebuluni akawa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 10. Eloni wa Zebuluni alipokufa akazikwa huko Ayaloni katika nchi ya Zebuluni. Baada yake Abudoni, mwana wa Hileli wa Piratoni, akawa mwamuzi wa Waisiraeli. Naye alikuwa mwenye wana 40 na wajukuu 30 waliopanda wana wa punda 70. Akawa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 8. Abudoni, mwana wa Hileli wa Piratoni, alipokufa akazikwa huko Piratoni katika nchi ya Efuraimu mlimani kwa Waamaleki. Wana wa Isiraeli walipoendelea kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, Bwana akawatia mikononi mwa Wafilisti miaka 40. Hapo palikuwa na mtu mmoja wa Sora wa ukoo wao Wadani, jina lake Manoa, mkewe huyu mtu alikuwa mgumba, hakuzaa. Huyu mwanamke akatokewa na malaika wa Bwana, akamwambia: Tazama, wewe u mgumba, hujazaa; lakini utapata mimba, uzae mtoto mwanamume. Sasa jiangalie, usinywe mvinyo wala kileo cho chote, wala usile chakula cho chote chenye mwiko. Kwani utajiona kuwa nwenye mimba, kisha utazaa mtoto mwanamume; nacho kinyoleo kisifike kichwani pake, kwani kijana huyo atakuwa ametengwa kuwa wake Mungu tangu hapo, atakapozaliwa. Naye ndiye atakayeanza kuwaokoa Waisiraeli mikononi mwa Wafilisti. Ndipo, yule mwanamke alipokwenda kumwambia mumewe kwamba: Mtu wa Mungu amekuja kwangu, nayo sura yake ilionekana kabisa kuwa kama sura ya malaika wa Mungu, naye alikuwa wa kutisha sana, kwa hiyo sikumwuliza, anakotoka, naye hakuniambia jina lake. Akaniambia: Utajiona kuwa mweye mimba, kisha utazaa mtoto mwanamume. Toka sasa usinywe mvinyo wala kileo cho chote, wala usile chakula cho chote chenye mwiko, kwani kijana huyo atakuwa ametengwa kuwa wake Mungu tangu hapo, atakapozaliwa hata siku ya kufa kwake. Ndipo, Manoa alipomlalamikia Bwana kwamba: E Bwana, yule mtu wa Mungu, uliyemtuma, na aje tena kwetu, atufundishe vema, tutakayomfanyizia huyo kijana atakayezaliwa. Mungu akaisikia sauti ya Manoa, yule malaika wa Mungu akaja mara ya pili kwa yule mwanamke, alipokuwa anakaa shambani, lakini mumewe Manoa alikuwa hayuko kwake. Ndipo, yule mwanamke alipopiga mbio na kukimbia sana, akampasha mumewe hiyo habari akimwambia: Tazama, amenitokea yule mtu aliyekuja kwangu siku hiyo. Ndipo, Manoa alipoondoka, akamfuata mkewe, akafika kwa yule mtu, akamwuliza: Wewe ndiwe yule mtu aliyesema na huyu mwanamke? Akasema: Ni mimi. Manoa akauliza: Sasa neno lako litakapotimia, yatakayompasa huyo kijana ndio nini? Tena kazi yake itakuwa nini? Malaika wa Bwana akamwambia Manoa: Huyu mwanamke sharti ayaangalie yote, niliyomwambia, ayafanye! Yote yatokayo katika mzabibu asiyale, wala asinywe mvinyo wala kileo cho chote! Wala asile chakula cho chote chenye mwiko! Yote, niliyomwagiza, sharti ayaangalie. Kisha Manoa akamwambia malaika wa Bwana: Tunataka kukushika, tukuandalie mwana mbuzi. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Manoa: Ijapo unishike, sitakila chakula chako; lakini ukitaka kutoa ng'ombe ya tambiko, mtolee Bwana ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Kwani Manoa hakujua, ya kuwa yeye ni malaika wa Bwana. Ndipo, Manoa alipomwuliza malaika wa Bwana: Jina lako nani, tupate kukuheshimu, neno lako litakapotimia? Malaika wa Bwana akamwambia: Unaniuliziaje jina langu? nalo ni la kustaajabu. Ndipo, Manoa alipochukua mwana mbuzi na kilaji cha tambiko, akamtolea Bwana juu ya mwamba hivyo vipaji vya tambiko; naye akafanya jambo la kustaajabu, nao Manoa na mkewe wakawa wanalitazama: Ikawa hapo pa kutambikia, miali ya moto ilipopanda mbinguni, ndipo, malaika wa Bwana naye alipopaa katika miali ya moto uliokuwapo hapo pa kutambikia; nao Manoa na mkewe walipoviona, ndipo, walipoanguka kifudifudi chini. Kisha malaika wa Bwana hakumtokea tena Manoa wala mkewe; ndipo, Manoa alipojua, ya kuwa ndiye malaika wa Bwana. Naye Manoa aakamwambia mkewe: Hatuna budi kufa, kwa kuwa tumemwona Mungu. Lakini mkewe akamwambia: Kama Mungu angependa kutuua, asingalipokea mikononi mwetu ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima pamoja na kilaji cha tambiko, wala asingalituonyesha hayo yote, wala asingalitupasha habari hizo zote wakati huo. Yule mwanamke alipozaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samusoni; huyu kijana alipokua, Bwana akambariki. Roho ya Bwana ilipoanza kumhimiza, alikuwa kambini kwao Wadani katikati ya Sora na Estaoli. Samusoni alipotelemka kwenda Timuna akaona huko Timuna mwanamke kwao vijana wa kike wa Wafilisti. Alipopanda kwao akamwambia baba yake na mama yake kwamba: Nimeona mwanamke huko Timuna kwao vijana wa kike wa Wafilisti, sasa mchukueni, awe mke wangu! Baba yake na mama yake wakamwambia: Kumbe kwetu hakuna mwanamke kwao vijana wa kike wa ndugu zako walio ukoo wetu, wewe ukienda kuchukua mwanamke kwao Wafilisti wasiotahiriwa? Lakini Samusoni akamwambia baba yake: Huyo mchukue, awe mke wangu! Kwani ndiye apendezaye machoni pangu. Lakini baba yake na mama yake hawakujua, ya kuwa shauri hili limetoka kwa Bwana, ya kuwa yeye alitafuta njia ya kuwajia Wafilisti, maana wakati huo Wafilisti waliwatawala Waisiraeli. Samusoni alipotelemka kwenda Timuna pamoja na baba yake na mama yake, hapo, walipofika kwenye mizabibu ya Timuna, mara mwana wa simba akamkingia njiani na kumngurumia. Mara roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, akamrarua, kama ni kurarua mwana mbuzi, lakini hakuwa na mata mkononi mwake. Lakini baba yake na mama yake hakuwasimulia, aliyoyafanya. Kisha akaenda Timuna kuongea na yule mwanamke, naye akapendeza zaidi machoni pake Samusoni. Siku zilipopita, akarudi kumchukua. Alipotoka njiani, aende kuutazama ule mzoga wa yule simba, akaona, nyuki wengi wa porini wamo ndani ya mzoga wa simba, hata asali imo. Akaitwaa mikononi mwake, akaendelea njiani akiila. Kisha akaenda kwao baba yake na mama yake, akawapa nao, nao wakaila, lakini hakuwaambia, ya kuwa asali hii ameitwaa katika mzoga wa simba. Baba yake alipotelemka kwenda kwa yule mwanamke, Samusoni akafanya huko karamu, kwani ndivyo, vijana walivyofanya. Ikawa, walipomwona wakachukua wenzake 30 wa kuwa naye. Samusoni akawaambia: Na niwategee kitendawili! Kama mtaniambia maana yake siku hizi saba za karamu kwa kuitambua maana, basi, nitawapa ninyi kanzu 30 na mavazi mengine 30. Lakini msipoweza kuniambia maana yake, ninyi mtanipa kanzu 30 na mavazi mengine 30. Wakamwambia: Kitege kitendawili chako, tukisikie! Akawaambia: Kwa mlaji kikatoka chakula, kwa mwenye nguvu kikatoka kitamu. Siku tatu hawakuweza kumwambia maana ya hicho kitendawili. Ikawa siku ya saba, wakamwambia mkewe Samusoni: Mnyege mumeo, atuambie hicho kitendawili, tusikuchome moto pamoja na nyumba ya baba yako! Je? Mmetualika kuja huku, mpate kuzichukua mali zetu! Au sivyo? Ndipo, mkewe Samusoni alipomlilia na kumwambia: Kumbe unachukizwa na mimi, hunipendi! Wana wao walio ukoo wangu umewategea kitendawili, lakini mimi hujaniambia. Akamwambia: Tazama, hata baba yangu na mama yangu sikuwaambia, wewe nitawezaje kukuambia? Alipomlilia hizo siku saba za karamu yao, basi, siku ya saba akamwambia maana, kwani alimsumbua sana, naye akawaambia hicho kitendawili wale wana wa ukoo wake. Kwa hiyo watu wa ule mji wakamwambia siku ya saba, jua lilipokuwa halijachwa bado: Kiko kitamu kuliko asali? Yuko mwenye nguvu kuliko simba? Naye akawaambia: Kama hamngalimtumia ndama wangu, hapo mlipolima, hicho kitendawili changu hamngaliona maana. Kisha roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, akatelemka kwenda Askaloni, akaua huko watu 30, akachukua yote, waliyokuwa nayo, nayo mavazi akawapa wao waliomwambia maana ya kitendawili, lakini makali yake yakawaka moto, aliporudi nyumbani mwa baba yake. Kisha mkewe Samusoni akawa mkewe mmoja wao wenzake, Samusoni aliyemchagua kuwa rafiki yake. Siku zilipopita, siku za mavuno ya ngano zilipokuwa karibu, Samusoni alikwenda kumwamkia mkewe na kumpa mwana mbuzi, akisema moyoni: Nitaingia chumbani kwa mke wangu. Lakini baba yake hakumpa ruhusa kuingia. Baba yake akamwambia: Nilidhani, umechukizwa naye, nikampa mwenzako; je? Ndugu yake mdogo si mwema kuliko yeye? Na awe wako mahali pake! Samusoni akawaambia: Mara hii sitakora manza kwao Wafilisti nikiwafanyizia mabaya. Kisha Samusoni akaenda, akakamata mbweha 300, kisha akachukua mienge yenye moto, akawafunga wawiliwawili mkia kwa mkia, akatia mwenge mmoja katikati ya mikia miwili. Tena alipokwisha kuiwasha moto ile mienge, akawaacha, waende mashambani kwa Wafilisti kwenye ngano; ndivyo, alivyozichoma hizo ngano zilizokwisha kufungwa miganda, nazo zilizokuwa mabuani bado, hata mizabibu na michekele. Wafilisti walipoulizana: Ni nani aliyeyafanya haya? watu wakasema: Ni Samusoni, mkwewe yule mtu wa Timuna, kwa kuwa amemchukua mkewe, akampa mwenzake. Ndipo, Wafilisti walipopanda huko, wakamteketeza kwa moto yule mwanamke pamoja na nyumba ya baba yake. Lakini Samusoni akawaambia: Mkifanya mambo kama hayo, kweli nitajipatia malipizi kwenu, kisha nitaacha. Akawapiga akitumia mguu wa mmoja wa kupigia kiuno cha mwingine, likawa pigo kubwa sana. Kisha akaenda kukaa katika pango la mwamba wa Etamu. Kisha Wafilisti wakapanda, wakapiga makambi katika nchi ya Yuda, wakajieneza huko Lehi. Wayuda walipowauliza: Mmetupandia kwa sababu gani? wakasema: Tumepanda, tumfunge Samusoni, tumfanyizie, kama alivyotufanyizia sisi. Ndipo, waliposhuka watu 3000 toka Yuda kwenda kwenye pango la mwamba wa Etamu, wakamwambia Samusoni: Kumbe hujui, ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Mbona unatufanyizia mambo kama hayo? Akawaambia: Kama walivyonifanyizia, ndivyo, nilivyowafanyizia nao. Wakamwambia: Tumekuja, tukufunge, tukutie mikononi mwa Wafilisti. Samusoni akawaambia: Niapieni, ya kuwa hamtanipiga ninyi, mniue! Nao wakamwambia kwamba: Hivyo sivyo, sisi tunataka tu, tukufunge, tukutie mikononi mwao, lakini hatutakuua kabisa. Kisha wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakampandisha kutoka pale mwambani. Yeye alipofika Lehi, Wafilisti wakamawendea njiani na kumzomea. Ndipo, roho ya Bwana ilipomjia kwa nguvu, nazo kamba, ambazo mikono ilifungwa nazo, zikawa kama nyuzi zilizounguzwa na moto, pingu zake nazo zikayeyuka na kuanguka mikononi pake. Alipoona hapo mfupa mbichi wa taya la punda, akapeleka mkono wake, akauchukua, akaua nao watu 1000. Kisha Samusoni akasema: Kwa taya la punda wanalala machungu, huku chungu moja, huko machungu mawili; kwa taya la punda nimewaua watu elfu zima. Alipokwisha kuyasema haya, akautupa huo mfupa wa taya, alioushika mkononi mwake; kwa hiyo watu wakapaita mahali pale Ramati-Lehi (Kilima cha Taya). Kisha akaona kiu kali, ndipo, alipomlilia Bwana akisema: Wokovu huu mkubwa umewapatia hawa kwa mkono wa mtumishi wako; sasa nife kwa kiu, nianguke mikononi mwao hao wasiotahiriwa! Ndipo, Mungu alipopasua shimo lililoko Lehi, mara yakatoka maji humo, naye akanywa, mpaka roho yake ikamrudia, akapata kuwa mzima tena. Kwa hiyo hapo huitwa Chemchemi ya Mliaji, nayo iko huko Lehi hata siku hii ya leo. Akawa mwamwuzi wa Waisiraeli miaka 20 siku zile za Wafilisti. Samusoni alipokwenda Gaza akaona huko mwanamke mgoni, akaingia kwake. Wagaza walipoambiwa, ya kuwa Samusoni ameingia humo, wakaizunguka hiyo nyumba na kumvizia usiku wote penye lango la mji, wakanyamaza kimya usiku kucha kwa kwamba: Tungoje mapambazuko ya asubuhi, tupate kumwua. Lakini Samusoni akalala mpaka usiku wa manane tu; hapo usiku wa manane ndipo, alipoondoka, akaishika milango ya lango la mji pamoja na miimo yake miwili, akaing'oa pamoja na komeo, akajitwika mabegani, akaipandisha mlimani kunakoelekea Heburoni. Ikawa baadaye, Samusoni akapenda mwanamke aliyekaa penye kijito cha Soreki, jina lake Delila. Ndipo, wakuu wa Wafilisti walipopanda kufika kwake, wakamwambia: Umnyenge, upate kuona, nguvu zake kubwa zilimo, tena utazame njia ya kumwona sisi, tupate kumfunga na kumshinda. Kisha tutakupa kila moja fedha elfu moja na mia moja. Ndipo, Delila alipomwambia Samusoni: Nijulishe, nguvu zako kubwa zilimo, tena ndivyo ufungwe navyo, watu wakushinde! Samusoni akamwambia: Kama wangenifunga kamba saba za mishipa zisizokauka bado, ningekuwa mnyonge kuwa kama kila mtu mwingine. Kisha wakuu wa Wafilisti wakampelekea kamba saba za mishipa zisizokauka bado, naye akamfunga nazo, watu waliokuwa wanamvizia wakikaa kwake chumbani. Kisha akamwambia: Wafilisti wanakujia, Samusoni; ndipo, alipozirarua hizo kamba, kama uzi wa madifu ukionja moto; lakini nguvu zake hazikujulikana. Kisha Delila akamwambia Samusoni: Tazama, umenidanganya, ukaniambia maneno ya uwongo, sasa nijulishe, ndivyo ufungwe navyo! Akamwambia: Kama wangenifunga kwa kamba mpya zisizotumika bado kazini, ningekuwa mnyonge kuwa kama kila mtu mwingine. Ndipo, Delila alipochukua kamba mpya, akamfunga nazo, akamwambia: Wafilisti wanakujia, Samusoni; lakini watu waliokuwa wanamvizia walikaa chumbani. Naye akazirarua hizo kamba mikononi pake kama uzi. Ndipo, Delila alipomwambia Samusoni; Mpaka sasa umenidanganya, ukaniambia maneno ya uwongo, sasa nijulishe, ndivyo ufungwe navyo! Akamwambia: Kama ungefuma shungi saba za kichwani pangu pamoja na nyuzi za mtande za kufuma nguo, basi. Alipokwisha kuzipigilia kwa uwambo akamwambia: Wafilisti wanakujia, Samusoni; ndipo, alipoamka katika usingizi, akaung'oa ule uwambo wa kufumia pamoja na nyuzi za mtande. Ndipo, alipomwambia: Unasemaje: Ninakupenda, moyo wako ukiwa hauko kwangu? Mara hizi tatu umenidanganya usiponijulisha, nguvu zako kubwa zilimo. Ikawa, alipozidi kumsumbua siku zote na hayo maneno yake kwa kumhimiza, mwisho roho yake ikalegea, atake kufa tu; ndipo, alipomjulisha yote yaliyokuwamo moyoni mwake, akamwambia: Hakijafika kinyoleo kichwani pangu, kwani mimi nilitengwa kuwa wake Mungu tangu hapo, nilipozaliwa na mama yangu. Kama ningenyolewa, nguvu zangu zingenitoka, niwe mnyonge kuwa kama kila mtu mwingine. Delila alipoona, ya kuwa amemjulisha yote yaliyokuwamo moyoni mwake, akatuma kuwaita watu wa Wafilisti kwamba: Pandeni mara hii tu! Kwani amenijulisha yote yaliyokuwamo moyoni mwake. Nao wakuu wa Wafilisti walipopanda kufika kwake walishika zile fedha mikononi mwao. Kisha akambembeleza, alale usingizi penye magoti yake; alipokwisha akaita mtu, naye akazinyoa zile chungu saba za kichwani pake; ndivyo, alivyoanza kumshinda, maana nguvu zake zilikuwa zimemtoka. Kisha akasema: Wafilisti wanakujia, Samusoni. Alipoamka katika usingizi, alisema moyoni: Nitatoka kama mara nyingine zote kwa kujinyosha tu, kwani hakujua, ya kuwa Bwana ameondoka kwake. Ndipo, Wafilisti walipomkamata, wakamchoma macho, wakamshusha kumpeleka Gaza, wakamfunga kwa minyororo miwili ya shaba, kisha akawa kifungoni akisaga unga. Lakini kwa hivyo, alivyonyolewa, nywele za kichwani pake zikaanza kuota tena. Wakuu wa Wafilisti walipokusanyika kufanya sikukuu ya tambiko kubwa ya mungu wao Dagoni wakamfurahia kwamba: Mungu wetu ametupa adui yetu Samusoni mikononi mwetu! Watu walipomwona wakamsifu mungu wao, kwani walisema: Mungu wetu ametupa adui yetu mikononi mwetu, ndiye aliyeiangamiza nchi yetu kwa kuua watu wengi wa kwetu. Mioyo yao ilipochangamka, wakasema: Mwiteni Samusoni, atuchezee! Wakamwita Samusoni na kumtoa kifungoni, awachezee. Walipomsimamisha katikati ya nguzo, Samusoni akamwambia kijana aliyemshika mkono: Niachie, nizipapase hizi nguzo zinazoishikiza nyumba hii, niziegemee! Nayo hiyo nyumba ilikuwa imejaa watu waume na wake, nao wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo, namo darini walikuwamo kama 3000 waume na wake, waliomtazama Samusoni, jinsi alivyocheza. Ndipo, Samusoni alipomlilia Bwana kwamba: Bwana Mungu, nikumbuke, unitie nguvu hii mara moja tu, Mungu wangu, niwalipishe hawa Wafilisti kwa mara moja macho yangu mawili! Kisha Samusoni akazikamata hizo nguzo mbili za katikati zilizoishikiza hiyo nyumba, akaziegemea moja kwa mkono wa kuume, moja kwa mkono wa kushoto. Kisha Samusoni akasema: Nami mwenyewe na nife pamoja na hawa Wafilisti. Naye alipoinama kwa nguvu, nyumba ikawaangukia wakuu na watu wote pia waliokuwamo. Hivyo wenye kufa, aliowaua kwa kufa akwake, wakawa wengi zaidi kuliko wao, aliowaua alipokuwa yuko mzima bado. Kisha ndugu zake nao wote wa mlango wa baba yake wakatelemka, wakamchukua, wakampeleka kwao, wakamzika katikati ya Sora na Estaoli kaburini mwa baba yake Manoa. Naye alikuwa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 20. Milimani kwa Efuraimu kulikuwa na mtu, jina lake Mika. Huyu akamwambia mama yake: Hizo fedha 1100, ulizochukuliwa, umemwapizia mwenye kuzichukua namo masikioni mwangu, basi, hizo fedha mimi ninazo, nimezichukua mimi. Ndipo, mama yake aliposema: Ubarikiwe na Bwana, mwanangu! Akamrudishia mama yake hizo fedha 1100 naye mama yake akasema: Hizi fedha nimezitoa kabisa kuwa mali za Bwana, zitoke mkononi mwangu kwa ajili ya mwanangu, atengeneze kinyago cha kuchongwa, nacho kivikwe mabati ya fedha. Kwa hiyo sasa nazirudisha kwako. Alipomrudishia mama yake hizo fedha, huyu mama yake akachukua fedha 200, akampa mfua fedha, akazitumia kutengeneza kinyago cha kuchongwa kilichovikwa mabati ya fedha, kikawekwa nyumbani mwa Mika. Ndivyo, Mika alivyopata nyumba ya mungu, akatengeneza nacho kisibau cha mtambikaji kuwa kinyago cha nyumbani, kisha mmoja wao wanawe Mika akamjaza gao, akawa mtambikaji wake. Siku zile hakuwako mfalme kwao Waisiraeli, kwa hiyo kila mtu huyafanya yanyokayo machoni pake yeye. Kulikuwa na kijana wa Beti-Lehemu wa Yuda uliokuwa wa ukoo wa Yuda, naye alikuwa Mlawi, lakini alikuwa mgeni huko. Kisha huyu mtu akaondoka katika mji wa Beti-Lehemu wa Yuda kwenda kukaa ugenini mahali, atakapopaona; naye akafika milimani kwa Efuraimu nyumbani kwa Mika alipokuwa anajiendea tu. Mika akamwuliza: Umetoka wapi? Naye akamwambia: Mimi ni Mlawi wa Beti-Lehemu wa Yuda, nimekwenda kukaa ugenini mahali, nitakapopaona. Mika akamwambia: Kaa kwangu, uniwie baba na mtambikaji! Nami nitakupa fedha kumi mwaka kwa mwaka, hata nguo za kuvaa na vyakula vya kukutunza nitakupatia. Huyu Mlawi kwanza alitaka kwenda zake, halafu ikampendeza huyu Mlawi kukaa kwa huyu mtu, kisha huyu kijana akawa kwake kama mwanawe mmoja. Mika akamjaza gao huyu Mlawi, ndipo, huyu kijana alipokuwa mtambikiaji wake, akakaa nyumbani mwa Mika. Naye Mika akasema: Sasa najua, ya kuwa Bwana atanifanyizia mema, kwa kuwa huyu Mlawi ni mtambikaji wangu. Siku zile hakuwako mfalme kwao Waisiraeli, tena siku zile wao wa shina la Dani walikuwa wanajitafutia fungu la nchi la kukaa, kwani mpaka siku hiyo fungu lao la nchi halijawaangukia katikati ya mashina ya Isiraeli. Kwa hiyo wana wa Dani wakatoa katika ukoo wao wote mzima watu watano wenye nguvu waliokuwa wa Sora na wa Estaoli, wakawatuma kuipeleleza nchi na kuichunguza wakiwaambia: Nendeni mwichunguze nchi hii! Walipofika milimani kwa Efuraimu kwenye nyumba ya Mika wakalala huko. Walipokuwa nyumbani mwa Mika, wakamtambua yule kijana wa Kilawi kwa msemo wake; ndipo, walipomwendea, wakamwuliza: Ni nani aliyekuleta huku? Tena wewe unafanya nini hapa? Uko na kazi gani hapa? Akawaambia: Mika amenifanyizia hivi na hivi, akanipa kazi hii ya mshahara kuwa mtambikaji wake. Wakamwambia: Mwulize Mungu, tujue, kama njia yetu, tunayokwenda sisi, itafanikiwa. Mtambikaji akawaambia: Nendeni na kutengemana! Njia yenu, mnayoishika, Bwana anaiona. Hao watu watano walipokwenda zao wakafika Laisi, wakaona, ya kuwa watu waliokuwamo walikaa na kutulia tu kama desturi za Wasidoni, walikaa kimya na kutulia kweli, kwani hakuwako katika nchi hiyo aliyewafanyizia kibaya cho chote, nao wote walikuwa wenye mali. Tena kutoka kwa Wasidoni kufika kwao kulikuwa mbali, hawakupata matata yo yote na watu wo wote. Walipofika kwa ndugu zao huko Sora na Estaoli, nao walipowauliza: Mnaleta habari gani? wakawaambia: Ondokeni, twende kupanda kwao hao! Kwani tulipoitazama hiyo nchi, tumeiona kuwa njema sana. Nanyi mnanyamaza tu! Msikawilie kwenda na kuiingia hiyo nchi, iwe yenu! Mtakapofika mtafika kwenye watu wanaokaa na kutulia, nayo nchi hiyo inapanuka pande mbili. Kweli Mungu ameitia mikononi mwenu, tena ni mahali pasipokoseka lo lote lililoko huku nchini. Ndipo, walipoondoka huko Sora na Estaoli watu 600 wa ukoo wa Dani, kila mtu akiwa amejifunga mata ya kupigia vita. Walipopanda wakapiga makambi Kiriati-Yerarimu wa Yuda; kwa hiyo watu huita mahali pale Makambi ya Dani hata siku ya leo, pako nyuma ya Kiriati-Yearimu. Walipotoka huko na kushika njia ya kweda milimani kwa Efuraimu wakafika kwenye nyumba ya Mika. Nao wale watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisi wakaanza kusema na ndugu zao, wakawaambia: Je? Mnajua, ya kuwa humu katika hizi nyumba kimo kisibau cha mtambikaji pamoja na kinyago cha nyumbani, nacho ni inyago cha kuchongwa kilichovikwa mabati ya fedha. Sasa lijueni la kufanya! Walipoondoka kwenda huko wakaingia nyumbani mwa yule kijana wa Kilawi kwenye nyumba ya Mika, wakaamkiana naye. Nao wale watu 600 waliojifunga mata ya kupigia vita, wale wana wa Dani, walikuwa wamesimama pa kuingia langoni. Nao wale watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi hii wakaingia humo, wakakichukua kile kinyago cha kuchongwa pamoja na kisibau cha mtambikaji, ni kile kinyago cha nyumbani kilichovikwa mabati ya fedha, naye mtambikaji alikuwa amesimama pa kuingia langoni kwao wale watu 600 waliojifunga mata ya kupigia vita. Wale watano walipoingia nyumbani mwa Mika, wakichukue kile kinyago cha kuchongwa pamoja na kisibau cha mtambikaji, ni kile kinyago cha nyumbani kilichovikwa mabati ya fedha, ndipo, mtambikaji alipowauliza: Mnafanya nini? Lakini wao wakamwambia: Nyamaza tu ukiubandika mkono wako kinywani pako, upate kwenda nasi kuwa baba yetu na mtambikaji wetu. Ni vema, ukiwa mtambikaji wa mlango wa mtu mmoja, kuliko ukiwa mtambikaji wa shina na wa ukoo mzima kwao Waisiraeli? Moyo wa mtambikaji ukayaona haya kuwa mema; ndipo, alipokichukua kisibau cha mtambikaji pamoja na kile kinyago cha nyumbani, ni kile kinyago cha kuchongwa, akaingia kwa hao watu katikati. Kisha wakageuka kwenda zao; lakini wanawake pamoja na watoto na nyama wa kufuga na vyombo vilivyokuwa mali walitangulia mbele yao. Walipokwisha kuiacha nyumba ya Mika mbali, watu waliokaa katika zile nyumba kwenye nyumba ya Mika wakaitana, wakusanyike, wakaenda kuandamana na wana wa Dani. Walipowaita wana wa Dani, wakazigeuza nyuso zao, wakamwuliza Mika: Una nini, mkikusanyika kwa kuitana? Akasema: Mmeichukua miungu yangu, niliyoitengeneza, pamoja na mtambikaji, mkajiendea. Sasa mimi niko na nini tena? Nanyi mnaniulizaje: Una nini? Nao wana wa Dani wakamwambia: Usitupigie kelele tena, watu wenye uchungu mioyoni wasije kwenu na kuwapiga ninyi, roho yako nazo roho zao walio wa mlango wako zisiangamizwe pamoja. Kisha wana wa Dani wakaenda zao, naye Mika alipoona, ya kuwa wao ni wenye nguvu za kumshinda yeye, akarudi nyumbani kwake. Nao wakavichukua vile, Mika alivyovitengeneza, pamoja na mtambikaji aliyekuwa kwake, wakaenda Laisi, kwenye wale watu waliokaa kimya na kutulia tu, wakawapiga kwa ukali wa panga, nao mji wakauteketeza kwa moto. Hakuwako aliyewaponya, kwani kwenda Sidoni toka kwao kulikuwa mbali, nao walikuwa hawana matata na watu wo wote; nao mji wao ulikuwa bondeni kuelekea Beti-Rehobu. Kisha wakaujenga huo mji tena, wakakaa humo. Lakini jina la mji wakaliita Dani kwa jina la baba yao Dani, Isiraeli aliyemzaa; lakini jina la kwanza la mji lilikuwa Laisi. Kisha wana wa Dani wakajisimamishia kile kinyago kilichochongwa, naye Yonatani, mwana wa Gersomu, mwana wa Mose, yeye pamoja na wanawe wakawa watambikaji wa shina la Dani mpaka siku hiyo, walipohamishwa kwenda katika nchi nyingine. Nao walikuwa wamejisimamishia hicho kinyago, Mika alichokitengeneza, siku hizo zote, Nyumba ya Mungu ilipokuwa huko Silo. Siku zile hakuwako mfalme kwao Waisiraeli. Kulikuwa na mtu wa Kilawi aliyekaa ugenini milimani kwa Efuraimu huko ndani, akajichukulia mwanamke wa Beti-Lehemu wa Yuda, awe suria. Lakini huyu suria akamfanyizia matata, akaondoka kwake kwenda nyumbani mwa baba yake huko Beti-Lehemu wa Yuda, akawa huko miezi minne. Ndipo, mumewe alipoondoka, akamfuata, aseme naye maneno ya kuugeuza moyo wake, apate kumrudisha; alikuwa anaye mtumishi wake na punda wawili. Yule kijana wa kike akamwingiza nyumbani mwa baba yake, naye baba yake alipomwona akafurahi kwa kukutana naye. Mkwewe, babake yule kijana wa kike, akamshika, akae naye siku tatu; wakala, wakanywa, wakalala huko. Siku ya nne wakaamka na mapema; alipotaka kuondoka, aende zake, babake yule kijana wa kike akamwambia mkwewe: Ushikize moyo wako kwa chakula kidogo, kisha mtakwenda zenu. Basi, wakakaa, wakala wao wawili pamoja, wakanywa, kisha babake yule kijana wa kike akamwambia huyu mtu: Afadhali ulale, moyo wako upate kuchangamka. Yule mtu alipoamka, aende zake, mkwewe akamhimiza kwa kumwomba, basi, akarudi, akalala huko. Siku ya tano akaamka na mapema, aende zake; lakini babake yule kijana wa kike akasema: Ushikize moyo wako, mkawilie, mpaka jua lipinduke. Wakala wao wawili. Yule mtu alipoondoka, aende zake, yeye na suria yake na mtumishi wake, mkwewe, babake yule kijana wa kike, akamwambia: Tazama, mchana umekwisha fikia kuwa jioni, afadhali ulale! Tazama, jua limekwisha kuchwa; lala hapa, moyo wako upate kuchangamka! Kesho mtajidamka kwenda zenu, ufike hemani kwako. Lakini yule mtu hakutaka kulala tena, akaondoka, akaenda zake, akafika ng'ambo ya Yebusi, ndio Yerusalemu; naye alikuwa na punda wake wawili waliotandikwa, hata suria yake alikuwa naye. Walipokuwa karibu ya Yebusi, mchana ulikuwa umekuchwa kabisa; ndipo, mtumishi alipomwambia bwana wake: Twende, tufike humu mjini mwa Wayebusi, tulale humo! Bwana wake akamwambia: Tusifikie mjini mwa wageni wasio wana wa Isiraeli, ila tuendelee, tufike Gibea. Kisha akamwambia mtumishi wake: Twende kufika katika mji mmoja wa hapa mbele, tulale Gibea au Rama. Wakashika njia kwendelea kwenda, nalo jua likawachwea, walipokuwa karibu ya Gibea wa Benyamini. Wakafika huko na kuingia mle Gibea, wapate mahali pa kulala. Walipokwisha kuingia na kukaa katika uwanja wa mji, hakuna mtu aliyewakaribisha nyumbani, wapate kulala. Mara wakaona mzee aliyechelewa, naye akatoka kazini kwake shambani; naye mtu huyu alikuwa wa milimani kwa Efuraimu, humo Gibea alikaa ugenini, maana wenyeji wa hapa walikuwa wana wa Benyamini. Alipoyainua macho yake akamwona yule mpitaji katika uwanja wa mji; ndipo, yule mzee alipomwuliza: Unakwenda wapi? Tena umetoka wapi? Akamwambia: Sisi tu wapitaji; tumetoka Beti-Lehemu wa Yuda, tunakwenda huko ndani milimani kwa Efuraimu, ndiko, nilikotoka; nalikwenda Beti-Lehemu wa Yuda, na sasa ninakwenda nyumbani mwa Bwana, lakini hakuna mtu aliyenikaribisha nyumbani. Tunayo mabua ya ngano na chakula kingine cha punda zetu, hata mikate na mvinyo mtumishi wako anayo ya kunitunza mimi na mjakazi wako na kijana huyu, hakuna ukosefu wa kitu cho chote. Mzee akamwambia: Tengemana tu! Yote unayoyakosa nitakupatia, usilale tu nje uwanjani! Akamwingiza nyumbani mwake, hata punda akawapa ya kula. Kisha wakaiosha miguu yao, wakala, wakanywa. Wao walipokuwa wanaichangamsha mioyo yao, mara watu wa mjini wasiofaa kitu wakaizunguka hiyo nyumba na kugonga mlangoni, wakamwambia mwenye nyumba, yule mzee kwamba: Mtoe huyo mtu aliyeingia nyumbani mwako, tumjue! Ndipo, mwenye nyumba alipotokea kwao, akawaambia: Ndugu zangu, hivi sivyo! Msifanye mabaya! Kwa kuwa mtu huyu ameingia nyumbani mwangu, msifanye upumbavu kama huu. Tazameni, yuko mwanangu wa kike, ni mwanamwali, tena yuko suria yake; hawa nitawatoa kwenu, mwakorofishe na kuwatendea yote, mtakayoyaona kuwa mema, lakini mtu huyu msimfanyizie upumbavu kama huu! Lakini hao watu wakakataa kumsikia; ndipo, yule mtu alipomkamata suria yake, akamtoa nje kwao. Nao walipomjua wakamfanyizia mabaya usiku kucha mpaka asubuhi; kulipopambazuka, ndipo, walipomwachia. Usiku ulipokucha, yule mwanamke akaja, akaanguka mlangoni penye nyumba ya yule mtu, bwana wake alimokuwa, akalala hapo chini, mpaka mchana ukitokea. Bwana wake alipoinuka asubuhi, akaifungua milango ya nyumba; tena alipotoka, ashike njia ya kwenda zake, mara akamwona suria yake vivyo hivyo, alivyokuwa ameanguka mlangoni penye nyumba, mikono yake ikishika kizingiti. Alipomwambia: Inuka, twende zetu! hakuna aliyejibu. Ndipo, alipomchukua na kumweka juu ya punda; ndivyo, yule mtu alivyoondoka kwenda kwao. Alipofika nyumbani mwake, akatwaa kisu, kisha akamshika suria yake, akamkata mifupa kwa mifupa kuwa vipande kumi na viwili, akavituma kufika mipakani po pote kwao Waisiraeli. Kila mtu aliyeviona akasema: Jambo kama hili halijafanyika, wala halijaonekana tangu siku hiyo, wana wa Isiraeli walipotoka Misri kwenda kupanda huku, mpaka siku hii ya leo. Haya! Liwekeni mioyoni mwenu, mpige mashauri, kisha mseme! Ndipo, wana wote wa Isiraeli walipotoka, mkutano wao ukamkusanyikia Bwana huko Misipa kuwa kama mtu mmoja toka Dani mpaka Beri-Seba, hata nchi ya Gileadi. Wote waliokuwa pembeni kwa watu wa mashina yote ya Waisiraeli wakatokea katika mkutano wao walio ukoo wa Mungu, watu 400000 waliokwenda kwa miguu waliojua kuchomoa panga. Nao wana wa Benyamini wakasikia, ya kuwa wana wa Isiraeli wamepanda kwenda Misipa. Ndipo, wana wa Isiraeli waliposema: Semeni, jinsi jambo hilo baya lilivyofanyika! Yule mtu wa Kilawi mwenye mwanamke aliyeuawa akajibu akisema: Naliingia Gibea wa Benyamini, mimi na suria yangu, tulale humo. Lakini wenyeji wa Gibea wakaniinukia; ulipokuwa usiku, wakaizunguka hiyo nyumba, nilimokuwa, wakataka kuniua mimi, naye suria yangu wakamkorofisha, mpaka akifa. Ndipo, nilipomshika suria yangu, nikamkata vipande, navyo nikavituma kufika mashambani po pote kwenye fungu la Waisiraeli, kwani walifanya mambo, Waisiraeli wanayoyawaza kuwa maovu na mapumbavu. Ninyi nyote wana wa Isiraeli mko hapa, sasa toeni maneno na mashauri yenu hapa! Ndipo, watu wote walipoinuka kama mtu mmoja kwamba: Hatutakwenda hata mmoja hemani kwake, wala hatutaondoka hata mmoja kwenda nyumbani kwake. Tutakalowafanyizia Wagibea hi hili: Tutawajia kwa kujipigia kura. Na tuchukue watu kumi wa kila mia ya mashina yote ya Waisiraeli, tena mia wa kila elfu na elfu wa kila elfu kumi, waende kuwachukulia watu pamba; watakaporudi, tutawafanyizia wao wa Gibea wa Benyamini yaupasayo huo upumbavu wote, waliowafanyia Waisiraeli. Ndivyo, watu wote wa Waisiraeli walivyokusanyikia huo mji wakiwa wameungwa kuwa kama mtu mmoja. Kisha mashina ya Waisiraeli wakatuma watu kwenda kwao mashina yote ya Benyamini kuwaambia: Hilo ni tendo baya gani lililofanyike kwenu? Sasa watoeni wale watu wasiofaa kitu waliomo Gibea, tuwaue, tuuondoe ubaya huo kwetu Waisiraeli! Lakini wana wa Benyamini wakakataa kuzisikia sauti za ndugu zao wana wa Isiraeli. Kisha wana wa Benyamini nao wakakusanyika Gibea na kutoka mijini mwao, waende vitani kupigana na wana wa Isiraeli. Wana wa Benyamini waliotoka mijini walipojikagua siku hiyo wlikuwa watu 26000 waliojua kuchomoa panga pasipo wenyeji wa Gibea waliokaguliwa kuwa watu wateule 700. Katika watu hawa wote walikuwa watu 700 waliochaguliwa kwa kuwa wenye shoto; kila mmoja wao alijua kutupa mawe kwa kombeo, asikose, ijapo uwe unywele tu, aliotaka kuupiga. Waisiraeli nao walipojikagua walikuwa watu 400000 waliojua kuchomoa panga pasipo Wabenyamini; hao wote walikuwa watu wa vita. Kisha Waisiraeli wakaondoka, wakapanda kwenda Beteli, wakamwuliza Mungu, wana wa Isiraeli wakisema: Ni wa nani wa kwetu, ndio waanze kupigana na wana wa Benyamini? Bwana akasema: Wayuda na waanze! Kisha wana wa Isiraeli wakaondoka asubuhi, wakapiga makambi yao kuelekea Gibea. Waisiraeli walipotoka kupigana wa Wabenyamini, Waisiraeli wakajipanga kupigana nao hapo Gibea. Wana wa Benyamini walipotoka Gibea, wakawafanyizia Waisiraeli vibaya siku hiyo na kulaza chini watu 22000. Lakini watu wa Waisiraeli wakajishupaza, wakajipanga tena kupigana papo hapo, walipojipanga siku ya kwanza. Lakini tena walikuwako wana wa Isiraeli waliopanda na kumlilia Bwana mchana kutwa, wakamwuliza Bwana kwamba: Tuendelee kujisogeza, tupigane na wana wa Benyamini walio ndugu zetu? Bwana akawaambia: Haya! Wapandieni! Wana wa Isiraeli walipowakaribia wana wa Benyamini siku ya pili, wana wa Benyamini wakatoka Gibea kukutana nao hiyo siku ya pili, wakawafanyizia wana wa Isiraeli vibaya na kulaza chini tena watu 18000, nao wote walikuwa watu waliojua kuchomoa panga. Ndipo, wana wote wa Isiraeli nao watu wote walipopanda kwenda Beteli, wakamlilia Bwana huko pasipo kukoma, wakafunga siku hiyo mchana kutwa wakimtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani. Kisha wana wa Isiraeli wakamwuliza Bwana; nazo siku hizo Sanduku la Agano la Mungu lilikuwako huko. Naye Pinehasi, mwana wa Elazari, mwana wa Haroni, alitumikia huko siku hizo. Wakauliza: Tuendelee kutoka kupigana na wana wa Benyamini walio ndugu zetu, au tuache? Bwana akasema: Pandeni! Kwani kesho nitawatia mikononi mwenu. Kwa hiyo Waisiraeli wakaweka wenye kuvizia po pote pande zote za Gibea. Wana wa Isiraeli walipowapandia wana wa Benyamini hiyo siku ya tatu wakajipanga kuelekea Gibea kama jana na juzi. Wana wa Benyamini nao wakatoka kukutana nao, wakatengekana na mji wa kwao; walipoanza kupiga watu wengine kama jana na juzi na kuwaumiza hapo barabarani watu wa Waisiraeli 30, palikuwa hapo, barabara moja inapokwenda kupanda Beteli, ya pili inakwenda Gibea na kupita mashambani. Basi, wana wa Benyamini wakasema: Hawa wanapigwa na sisi kama hapo kwanza. Lakini wana wa Isiraeli walisema: Na tukimbie, tuwatenge na mji wa kwao tukiwapeleka barabarani. Kwa hiyo Waisiraeli wote wakaondoka mahali pao kwenda kujipanga tena Baali-Tamari; papo hapo Waisiraeli waliovizia wakatoka upesi hapo, walipokuwa, upande wa machweoni kwa jua wa huko Geba. Ndivyo, watu 10000 waliochaguliwa katika Waisiraeli wote walivyoujia Gibea toka ng'ambo ya huko; ndipo, mapigano yalipokuwa makali, nao walikuwa hawajajua bado, ya kuwa mambo mabaya yamewapata. Ndivyo, Bwana alivyowapiga Wabenyamini mbele ya Waisiraeli, nao wana wa Isiraeli wakawafanyizia Wabenyamini mabaya siku hiyo kwa kuangamiza watu 25100, nao hao wote walijua kuchomoa panga. Ndipo, wana wa Benyamini walipoona, ya kuwa wamekwisha kupigwa. Lakini Waisiraeli waliendelea kuwaachia Wabenyamini mahali pao, walipokuwa, kwani waliwaegemea wao waviziao, waliowaweka ng'ambo ya huko ya Gibea. Nao waviziao wakajihimiza, waushambulie mji wa Gibea; wao waviziao walipouteka wakawaua wote waliokuwamo mjini kwa ukali wa panga. Nao Waisiraeli walikuwa wameagana nao waviziao kielekezo, kwamba wapandishe moshi mwingi kama wingu mle mjini. Ikawa, Waisiraeli walipogeuka hapo penye mapigano, Wabenyamini walipoanza kuwapiga Waisiraeli na kuumiza kama watu 30 wakasema: Kweli wanapigwa mbele yetu kama katika mapigano ya kwanza. Mara kile kielekezo cha moto kikaanza kupanda juu, lile wingu la moshi; nao Wabenyamini walipogeuka nyuma yao, wakaona, mji wote mzima ulivyoteketea na kupandisha moshi mbinguni. Ndipo, Waisiraeli walipogeuka, nao Wabenyamini wakastushwa, kwani waliona, ya kuwa mabaya yamekwisha kuwapata. Ndipo, walipogeuka na kuwaonyesha Waisiraeli migongo yao, wakashika njia ya kwenda nyikani; lakini mapigano yakaandamana nao, nao waliotoka mijini wakawaangamiza katikati yao. Wakawazunguka Wabenyamini kwa kuwafukuza, walipopumzika, wakawakimbiza mpaka ng'ambo ya Gibea ya upande wa maawioni kwa jua. Wakauawa kwao Wabenyamini 18000, nao hao wote walikuwa watu wenye nguvu. Ndipo, walipogeuka kukimbilia nyikani kwenye mwamba wa Rimoni; lakini wale wakawaokoteza barabarani na kuua tena 5000, wakagandamana nao kwa kuwafuata hata Gidomu, huko nako wakaua wengine wao 2000. Ndivyo, hesabu ya Wabenyamini wote walioangushwa ilivyokuwa siku hiyo watu 25000 waliojua kuchomoa panga, nao hao wote walikuwa watu wenye nguvu. Lakini watu 600 waliogeuka wakakimbilia nyikani, wakakaa kwenye mwamba wa Rimoni miezi minne. Kisha Waisiraeli wakawarudia wana wa Benyamini, wakawapiga kwa ukali wa panga wote walioonekana, watu wa mijini pia hata nyama; nayo miji yote iliyopatikana wakaiteketeza kwa moto. Waisiraeli walikuwa wameapa huko Misipa kwamba: Mtu wa kwetu asimpe mtu wa Benyamini mwanamke wa kike kuwa mkewe! Watu walipofike Beteli na kukaa huko mchana kutwa mbele ya Mungu, wakapaza sauti zao, wakalia kilio kikubwa na kusema: Bwana Mungu wa Isiraeli, kwa sababu gani hili limefanyika kwa Waisiraeli, shina moja likiwa limepotea leo kwetu Waisiraeli? Ikawa kesho yake, watu walipoamka na mapema, wakajenga hapo pa kutambikia, kisha wakatoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani. Ndipo, wana wa Isiraeli walipoulizana: Je? Katika mashina yote ya Waisiraeli wako wasiopanda kumtokea Bwana penye mkutano huu hapa Misipa? Kwani walikuwa wameapiana kiapo kikuu cha kwamba: Wao watakaokaa, wasipande kumtokea Bwana, hawana budi kuuawa. Tena wana wa Isiraeli wakawaonea uchungu ndugu zao Wabenyamini, wakasema: Leo hivi shina moja limekatwa kwetu Waisiraeli. Tufanyeje, wao waliosalia tuwapatie wanawake? Kwani sisi tumeapa na kumtaja Bwana, tusiwape wana wetu wa kike kuwa wake zao. Wakaulizana tena: Je? Miongoni mwa mashina ya Waisiraeli liko moja lisilopanda kumtokea Bwana hapa Misipa? Ndipo, ilipoonekana, ya kuwa watu wa Yabesi wa Gileadi hawakuja makambini kwenye mkutano huu. Watu walipojikagua wakaona: Kweli kwao wenyeji wa Yabesi wa Gileadi hakuja hata mmoja. Ndipo, watu wa mkutano walipochagua kwao walio wenye nguvu watu 12000, wakawatuma kwenda huko wakiwaagiza kwamba: Nendeni, mwapige wenyeji wa Yabesi wa Gileadi kwa ukali wa panga, hata wanawake na watoto! Tena hivi ndivyo mfanye: kila mume mtamtia mwiko wa kuwapo, vilevile kile mwanamke aliyekwisha kutambua mtu mume. Lakini kwao wenyeji wa Yabesi wa Gileadi wakaonekana wanawali 400 wasiotambua bado mtu mume kwa kulala naye; hao wakawapeleka katika makambi ya Silo ulioko katika nchi ya Kanaani. Kisha watu wote wa mkutano wakatuma wengine kwenda kwa wana wa Benyamini huko mwambani kwa Rimoni, wawaambie, ya kuwa vita vimekwisha. Ndipo, Wabenyamini waliporudi kwao wakati huo, nao wale wakawapa wale wanawake wa Yabesi wa Gileadi, walioacha kuwaua, lakini hawakuwatoshea. Nao watu wakawaonea Wabenyamini uchungu, kwa kuwa Bwana amewatenga Waisiraeli, patokee ufa. Wazee wa mkutano wakasema: Tufanyeje, tuwapatie wanawake nao wale waliosalia? Kwani kwa Wabenyamini wanawake walikuwa wameangamizwa. Wakasema: Fungu zima la nchi ni lao Wabenyamini waliopona, lisitoweke shina moja kwetu Waisiraeli. Lakini sisi hatuwezi kuwapa wana wetu wa kike kuwa wake zao, kwani sisi wana wa Isiraeli tumeapa kwamba: Aapizwe atakayempa Mbenyamini mwanamke! Kisha wakasema: Tazameni! Mwaka kwa mwaka iko sikukuu ya Bwana huko Silo ulioko karibu ya Beteli upande wa kaskazini, ni hapo penye barabara itokayo Beteli kwenda Sikemu upande wa maawioni kwa jua, tena ni karibu ya Lebona upande wa kusini. Basi, wakawaagiza wana wa Benyamini kwamba: Nendeni kuvizia mizabibuni! Hapo, mtakapoona, vijana wa kike wa Silo wakitoka kucheza hiyo michezo, ndipo, mtakapotoka mizabibuni, mjikamatie kila mtu mkewe kwa hao vijana wa Silo! Kisha mwende zenu katika nchi ya Benyamini. Kama baba zao au ndugu zao watakuja kutugombeza, tutawaambia: Waacheni kuwa matunzo, mnayotupa sisi, kwa kuwa vitani hatukumpatia kila mtu mkewe. Hivyo ninyi hamtawatoa kuwapa wale; kama mngewapa wenyewe, mngekora manza. Wana wa Benyamini wakavifanya hivyo, wakachukua wanawake na kuwanyang'anya kwa hesabu yao kwao waliocheza michezo yao, kisha wakaenda zao, wakarudi katika nchi iliyokuwa fungu lao, wakajenga miji, wakakaa humo. Kisha wana wa Isiraeli wakaondoka huko, wakaenda kila mtu kwa shina lake na kwa ukoo wake. Ndivyo, walivyotoka huko kila mtu kwenda mahali pake palipokuwa fungu lake. Siku zile hakuwako mfalme kwao Waisiraeli, kwa hiyo kila mtu aliyafanya yanyokayo machoni pake yeye. Ikawa katika siku zile, waamuzi walipoamua, palikuwa na njaa katika nchi hiyo. Ndipo, mtu alipoondoka Beti-Lehemu wa Yuda kwenda kukaa ugenini katika mbuga za Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili wa kiume. Jina lake huyu mtu alikuwa Elimeleki, nalo jina lake mkewe alikuwa Naomi, nayo majina ya wanawe wa kiume walikuwa Maloni na Kilioni, ni Waefurati wa Beti-Lehemu wa Yuda. Walipofika kwenye mbuga za Moabu wakakaa huko. Kisha Elimeleki, mumewe Naomi, akafa, akaachwa yeye na wanawe wawili. Nao wakajichukulia wanawake wa Kimoabu, mmoja jina lake Orpa, wa pili jina lake Ruti, wakakaa huko kama miaka kumi. Ndipo, wote wawili Maloni na Kilioni walipokufa, yule mwanamke akasalia yeye tu kwa kufiwa na wanawe wawili na mumewe. Kisha akaondoka yeye na wakwewe, atoke kwenye mbuga za Moabu kurudi kwao, kwani alisikia kule kwenye mbuga za Moabu, ya kuwa Bwana amewakagua walio ukoo wake na kuwapa vyakula. Akatoka mahali hapo, alipokuwa, pamoja na wakwewe wawili, wakashika njia kwenda kurudi katika nchi ya Yuda. Naomi akawaambia wakwewe wawili: Nendeni kurudi kila mtu nyumbani mwa mama yake! Bwana awafanyizie mema, kama mlivyowafanyizia mema wanangu waliokufa, hata mimi. Bwana awape, mpate kutulia kila mmoja nyumbani mwa mumewe. Alipowanonea, wakazipaza sauti zao, wakalia machozi. Wakamwambia: Tutarudi pamoja na wewe kwa watu wa ukoo wako. Naomi akawaambia: Rudini, wanangu! Sababu gani mnataka kwenda na mimi? Niko na wana bado tumboni mwangu, wawe waume wenu? Rudini, wanangu, kwenda zenu! Kwani mimi ni mzee, siwezi kupata tena mume. Ijapo niseme: Niko na kingojeo, usiku huu wa leo nipate mume, nizae wana wa kiume, je? Ninyi mngeweza kuvumilia, mpaka wakiwa wakubwa? Mngeweza kufungiwa, kwa kuwa hamna waume? Msifanye hivyo, wanangu! Kwani naona uchungu mwingi sana kwa ajili yenu, kwa kuwa mkono wa Bwana umenitokea. Ndipo, walipozipaza sauti zao tena, wakalia machozi. Kisha Orpa akamnonea mkwewe, lakini Ruti akaandamana naye. Akamwambia: Tazama, dada yako amerudi kwao na kwa Mungu wao; rudi nawe kumfuata dada yako! Ruti akamwambia: Usinihimize kukuacha na kwenda kwetu, nisikufuate! Kwani uendako, ndiko, nitakakokwenda nami; ukaako, ndiko, nitakakokaa nami. Ukoo wako ni ukoo wangu, Mungu wako ni Mungu wangu. Utakakokufa, ndiko, nitakakofia, tena ndiko, ninakotaka kuzikwa; Bwana na anifanyizie hivi na hivi na kuendelea hivyo, kwani ni kufa tu kutakako tutenga mimi na wewe. Alipomwona, ya kuwa amejishupaza kwenda naye, akaacha kusema naye. Wakaenda wao wawili, mpaka wakifika Beti-Lehemu. Ikawa, walipofika Beti-Lehemu, mji wote ukavurugika kwa ajili yao wakisema: Kumbe huyu siye Naomi? Akawaambia: Msiniite Naomi (Apendezaye), ila mniite Mara (Mwenye uchungu). Kwani Mwenyezi amenifanyizia yenye uchungu sana. Nilipokwenda nilikuwa mwenye mali, lakini Bwana amenirudisha mikono mitupu. Mbona mnaniita Naomi? Naye Bwana ametoa ushuhuda wa kunishinda, yeye Mwenyezi ameniumiza vibaya. Ndivyo, Naomi alivyorudi pamoja na Ruti, mkwewe wa Kimoabu, alipotoka kwenye mbuga za Moabu kurudi kwao, nao wakafika Beti-Lehemu, mavuno ya mawele yalipoanza. Kulikuwa na mtu aliyekuwa fundi wa vita mwenye nguvu, naye alijuana sana na mumewe Naomi, alikuwa wa mlango wa Elimeleki, jina lake Boazi. Ruti wa Moabu akamwambia Naomi: Na niende shambani kuokoteza masuke nikimfuata mtu, nitakayempendeza machoni pake. Akamwambia: Nenda, mwanangu! Akaenda, akaja kuokoteza shambani akiwafuata wavunaji. Ikatukia kwa bahati, lile fugu la shamba kuwa lake Boazi aliyekuwa wa mlango wa Elimeleki. Ndipo, Boazi alipokuja toka Beti-Lehemu, akawaambia wavunaji: Bwana awe nanyi! Wakamwitikia: Bwana akubariki! Boazi akamwuliza kijana aliyewasimamia wavunaji: Huyu kijana wa kike ni wa nani? Yule kijana aliyewasimamia wavunaji akamjibu akimwambia: Huyu ni kijana wa Kimoabu aliyerudi na Naomi, alipotoka kwenye mbuga za Moabu. Alituambia: Na niokoteze na kukusanyakusanya penye miganda nikiwafuata wavunaji. Basi, akaja, akashinda hapa tangu asubuhi mpaka sasa; sasa anapumzika kidogo pale penye dungu. Ndipo, Boazi alipomwambia Ruti: Sikia, mwanangu! Usiende kuokoteza shambani pengine, wala usiondoke hapa, fuatana tu na vijana wa kwangu! Elekeza macho tu shambani, wanapovuna, uwafuate! Nimewaagiza hawa vijana, wasikusumbue. Ukiona kiu, nenda tu kwenye vyombo vyao, kanywe vijana hawa waliyoyachota! Ruti akamwangukia usoni pake na kumwimamia hapo chini, akamwambia: Mbona nimekupendeza machoni pako, unionee mema? Nami ni mgeni. Boazi akamjibu, akamwambia: Nimesimuliwa yote pia, uliyomfanyizia mkweo, mumeo alipokwisha kufa, ya kuwa umemwacha baba yako na mama yako na nchi, uliyozaliwa, ukaja kwa ukoo wa watu, usiowajua zamani zote. Bwana na akurudishie hayo matendo yako, upate mshahara wako wote mzima kwake Bwana Mungu wa Isiraeli, kwa kuwa umekuja kumkimbilia mabawani pake. Akamjibu: Kumbe nimekupendeza machoni pako, bwana wangu, ukanituliza moyo, ukaniambia maneno yaliyoingia moyoni mwa kijakazi wako, nami si kama mmoja wao hawa vijakazi wako! Saa wanapolia chakula, Boazi akamwambia: Karibu hapa, ule huku chakulani, nacho kitonge chako ukichovye hapa sikini! Akakaa kando ya wavunaji, naye akamgawia bisi, akala, hata akishiba, nyingine akazisaza. Alipoondoka kwenda kuokoteza, Boazi akawaagiza vijana wake kwamba: Hata katikati ya miganda na aokoteze, msimkaripie. Namo migandani mtoe mengine, myaache, aje kuyaokoteza, msimkaripie. Akaokoteza shambani mpaka jioni, akayapura maokotezo yake, yakawa kama frasila ya mawele. Akayachukua, akaja mjini. Mkwewe alipoyaona hayo maokotezo yake, akayatoa nayo, aliyoyasaza hapo, alipokula na kushiba, akampa. Mkwewe akamwuliza: Umeokoteza wapi leo? Umekwenda wapi kufanya kazi? Aliyekuonea mema na abarikiwe! Akamsimulia mkwewe, kama ni nani, ambaye amezifanya kazi zake kwake, akasema: Jina la huyo mtu, ambaye nimezifanya leo kazi zangu kwake, ndiye Boazi. Ndipo, Naomi alipomjibu mkwewe: Na abarikiwe na Bwana! Kwa kuwa hakuacha kuwatolea mema, wala wazima, wala wafu. Naomi akamwambia tena: Mtu huyo ni ndugu yetu, naye ni mmoja wa waingiliaji wetu. Ruti wa Moabu akamwambia: Tena ameniambia: Fuatana na hawa vijana wa kwangu, mpaka watakapoyamaliza mavuno yangu! Naomi akamjibu mkwewe Ruti: Inafaa, mwanangu, ukitoka pamoja na vijakazi wake, wasikukaripie halafu shambani. Basi, akafuatana na vijakazi wa Boazi kwenda kuokoteza, mpaka walipoyamaliza mavuno ya mawele na mavuno ya ngano; kisha akakaa kwa mkwewe. Naomi akamwambia mkwewe: Mwanangu, hainipasi kukutafutia mahali pa kutulia patakapokufaa? Tena Boazi siye ndugu yetu? ni yule, ambaye ulikuwa na vijakazi wake. Tazama, usiku wa leo Boazi anayapura mawele pake pa kupuria. Nenda koga na kujipaka mafuta, kisha vaa nguo zako nzuri, uende kushukia hapo pa kupuria, lakini uangalie, usijulikane kwake yule mtu, mpaka atakapokwisha kula na kunywa! Akienda kulala, upajue, atakapolala. Kisha uingie, uifunue miguu yake, upate kulala nawe; ndipo, atakapokuambia la kufanya wewe. Akamjibu: Yote, uliyoniambia, nitayafanya. Akashukia hapo pa kupuria, akayafanya yote, mkwewe aliyomwagiza. Boazi akala, akanywa, moyo wake ukachangamka, kisha akaenda kulala nyuma ya chungu la miganda. Ndipo, alipokwenda hapo polepole, akaifunua miguu yake, akalala naye. Ilipokuwa usiku wa manane, yule mtu akakupuka usingizini, akajiinua, mara akamwona mwanamke aliyelala miguuni pake. Akamwuliza: Wewe nani? Akasema: Mimi ni kijakazi wako Ruti; nawe umtandazie kijakazi wako pembe la blanketi lako! Kwani wewe ndiwe mwingiliaji. Akamjibu: Na ubarikiwe na Bwana, mwanangu! Haya mema yako ya nyuma, uliyoyafanya, yanayapita ya kwanza kwa wema, usipowafuata vijana, kama ni maskini au kama ni wenye mali. Sasa mwanangu, usiogope! Yote, utakayoniambia, nitakufanyizia; kwani watu wangu wote waliomo malangoni mwangu wanakujua wewe kuwa mwanamke mwema sana. Sasa hii ni kweli, mimi ni mwingiliaji; lakini yuko mwingiliaji mwenzangu anayepaswa nanyi kuliko mimi. Usiku huu lala hapa! Kesho asubuhi itajulikana: akiwa anataka kukuingilia, basi, ni vema, na akuingilie! Lakini akiwa hataki kukuingilia, mimi nitakuingilia kwa hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima! Lala tu, mpaka kuche! Akalala miguuni pake, hata kulipokucha; akaamka hapo, mtu asipoweza bado kumtambua mwenzake; Boazi akamwambia: Isijulikane, ya kuwa mwanamke amefika hapa pa kupuria! Akasema: Lete kanga, uliyojifunika, uishike! Akaishika, akampimia pishi sita za mawele, akamtwika, kisha akaenda zake mjini. Ruti alipoingia kwa mkwewe, akamwuliza: Habari gani, wewe mwanangu? Akamsimulia yote, yule mtu aliyomfanyizia. Kisha akasema: Amenipa hizi pishi sita za mawele, kwani aliniambia: Usiende mikono mitupu kwa mkweo. Naye akamwambia: Kaa tu, mwanangu, mpaka utakapolijua hilo jambo, litakavyoendelea. Kwani yule mtu hatatulia, asipolimaliza leo hilo jambo. Boazi akapanda kwenda langoni pa mji, akakaa huko. Mara yule mwingiliaji, Boazi aliyemtaja, akapita; ndipo, alipomwambia: Njoo, wewe bwana fulani, ukae hapa! Akaacha kwenda, akaja kukaa. Kisha akachukua watu kumi walio wazee wa mjini, akawaambia: Kaeni hapa! Nao wakakaa. Akamwambia huyo mwingiliaji: Fungu la shamba lililokuwa lake ndugu yetu Elimeleki, Naomi aliyerudi kutoka kwenye mbuga za Moabu anataka kuliuza. Nami nimesema, niyaeleze masikioni pako kwamba: Linunue machoni pao wanaokaa hapa napo machoni pao wazee wa ukoo wangu! Kama unataka kulikomboa, haya! Likomboe! Kama hutaki kulikomboa, niambie, nijue! Kwani kuliko wewe hakuna awezaye kulikomboa, mimi mwenyewe ni nyuma yako. Akasema: Basi, mimi nitalikomboa. Boazi akamwambia: Siku, utakapolinunua hilo shamba mkononi mwa Naomi na mwa Ruti wa Moabu, umempata naye huyo mke wake yeye aliyekufa, ulikalishe jina lake aliyekufa katika fungu lake. Ndipo, yule mwingiliaji aliposema: Sitaweza kulikomboa, liwe langu, nisiliharibu fungu langu. Likomboe wewe, liwe lako lililonipasa mimi, nilikomboe. Kwani siwezi kulikomboa. Tena kale kwa Waisiraeli ilikuwa desturi, walipokomboa, au waliponunua shamba, wakitaka kulishupaza hilo jambo la namna hii, mtu avue kiatu chake kimoja, ampe mwenzake; huu ulikuwa ushuhuda kwao Waisiraeli. Kwa hiyo, yule mwingiliaji alipomwambia Boazi: Linunue, liwe lako! akakivua kiatu chake. Ndipo, Boazi alipowaambia wale wazee nao watu wote: Ninyi m mashahidi leo hivi, ya kuwa nimeyapata mkononi mwa Naomi yote yaliyokuwa yake Elimeleki nayo yote yaliyokuwa ya Kilioni na ya Maloni. Naye Ruti wa Moabu, mkewe Maloni, nimempata, awe mke wangu, nilikalishe jina lake aliyekufa katika fungu lake, hilo jina lake aliyekufa lisiangamie kwa ndugu zake wala malangoni mahali pake, alipokuwa. Ninyi m mashahidi leo hivi. Ndipo, watu wote waliokuwako malangoni nao wazee wale waliposema: Tu mashahidi. Bwana na amfanye huyu mwanamke aliyeingia nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea walioijenga wote wawili nyumba ya Isiraeli! Pata nguvu mle Efurata, jina lako litajwe mle Beti-Lehemu! Nao mlango wako uwe kama mlango wa Peresi, Tamari aliyemzalia Yuda, nao utoke katika wazao, Bwana atakaokupa kwa kijana huyu! Ndivyo, Boazi alivyomchukua Ruti, akawa mkewe, akaingia nyumbani mwake, Bwana akampa kuwa mwenye mimba, akazaa mtoto wa kiume. Ndipo, wanawake walipomwambia Naomi: Bwana na atukuzwe, kwa kuwa hakukuacha leo, ukose mwingiliaji. Jina lake huyu na litangazwe kwao Waisiraeli, naye na akutulize roho yako kwa kukutunza vema katika uzee wako. Kwani mkweo anayekupenda, akufanyiziaye mema kuliko wana saba wa kiume, ndiye aliyemzaa. Kisha Naomi akamchukua yule mtoto, akamweka kifuani pake, akawa mlezi wake. Nao wanawake wenzake, waliokaa nao, wakamwita jina kwamba: Naomi amezaliwa mwana wa kiume, wakamwita jina lake Obedi (Mtumishi), naye ni babake Isai aliye babake Dawidi. Hawa ndio walio wa uzao wa Peresi: Peresi alimzaa Hesironi, Hesironi akamzaa Ramu, Ramu akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nasoni, Nasoni akamzaa Salmoni, Salmoni akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obedi. Obedi akamzaa Isai, Isai akamzaa Dawidi. Kulikuwa na mtu mmoja wa Ramataimu-Sofimu ulioko milimani kwa Efuraimu, jina lake ni Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, mtu wa Efuraimu. Naye alikuwa na wanawake wawili, mmoja jina lake Hana, wa pili jina lake Penina; huyu Penina alikuwa ana watoto, naye Hana alikuwa hana watoto. Yule mtu alitoka mwaka kwa mwaka mjini kwake akipanda kwenda Silo kumtambikia Bwana Mwenye vikosi na kumtolea ng'ombe ya tambiko. Huko wana wawili wa Eli, Hofuni na Pinehasi, walikuwa watambikaji wa Bwana. Kila siku, Elkana alipotoa ng'ombe ya tambiko, akampa mkewe Penina na wanawe wa kiume na wa kike vipande vya nyama. Naye Hana akampa kipande kimoja mara mbili, kwani alimpenda Hana, lakini Bwana alikuwa amelifunga tumbo lake. Naye mchukivu wake akamsikitisha sana kwa kumchokoza, kwa kuwa Bwana alilifunga tumbo lake. Ndivyo, alivyofanya mwaka kwa mwaka: kila alipopanda kuingia Nyumbani mwa Bwana, yule alimsikitisha, hata akalia machozi na kukataa kula. Ndipo, Elkana alipomwuliza mkewe Hana: Mbona unalia? Mbona huli nyama? Mbona moyo wako unakuwa mbaya hivyo? Kumbe mimi si mwenzio mwema kuliko wana kumi? Walipokwisha kula na kunywa huko Silo, Hana akaondoka; naye mtambikaji Eli alikwa amekaa katika kiti chake penye mhimili wa mlango wa Jumba la Bwana. Roho yake Hana ilikuwa yenye uchungu, akamlalamikia Bwana na kulia machozi mengi; akaaga kiagio na kusema: Bwana Mwenye vikosi, kama utautazama ukiwa wa kijakazi wako, ukinikumbuka, usimsahau kijakazi wako ukimpa kijakazi wako mwana wa kiume, nitamtoa, awe wako, Bwana, siku zote za maisha yake, nacho kinyoleo hakitafika kichwani pake. Ikawa, alipozidi kumlalamikia Bwana, Eli alikuwa anakiangalia kinywa chake. Lakini Hana alikuwa anasema humo ndani moyoni mwake, midomo yake ikachezacheza tu, lakini sauti yake haikusikilika; ndipo, Eli alipomwazia kuwa amelewa. Eli akamwambia: Utalewa mpaka lini? Acha, mvinyo, uliyoinywa, ikuondokee! Hana akajibu na kumwambia: Sivyo, bwana, mimi ni mwanamke mwenye roho nzito, mvinyo au kileo cho chote sikunywa, nitammwagia Bwana roho yangu tu. Usimwazie kijakazi wako kuwa mwanamke asiyefaa! Kwani hata sasa nimesema kwa wasiwasi na kwa uchungu wangu mwingi. Eli akajibu na kumwambia: Nenda na kutengemana! Mungu wa Isiraeli na akupe maombo yako, uliyomwomba. Akasema: Kijakazi wako na ayaone macho yako, yakimtazama kwa upole. Kisha huyo mwanamke akaenda zake, hata kula akala, nao uso wake haukuwa tena kama hapo kwanza. Kesho yake wakaamka na mapema, wakaja kumwangukia Bwana, kisha wakarudi kwenda nyumbani kwao huko Rama. Elkana alipomtambua mkewe Hana, Bwana naye akamkumbuka. Ikawa, siku zilipotimia, Hana akapata mimba, akazaa mtoto mwanamume, akamwita jina lake Samweli (Nimesikiwa na Mungu) kwa kwamba: Nimemwomba kwa Bwana. Kisha yule Elkana alipopanda pamoja nao wote walio wa mlango wake kumtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya zile siku, walizomwagia, Hana hakupanda nao, kwani alimwambia mumewe: Sharti huyu mwana kwanza aliache ziwa Kisha nitampeleka, amtokee Bwana usoni pake, akae hapo siku zote. Mumewe Elkana akamwambia: Yafanye yaliyo mema machoni pako! Kaa, mpaka umzoeze kuacha kunyonya! Naye Bwana na alitimize neno lako. Ndipo, mama ya mtoto alipokaa na kumnyonyesha mwanawe, mpaka akimzoeza kuacha kunyonya. Kisha akapanda naye, alipokwisha kumzoeza kuacha kunyonya, akachukua hata ng'ombe watatu na kapu moja la unga na kiriba cha mvinyo, akampeleka Silo Nyumbani mwa Bwana, yule mtoto akingali mdogo. Wakachinja ng'ombe, kisha wakampeleka yule mtoto kwa Eli. Hana akamwambia: Bwana, hivyo roho yako, bwana wangu, ilivyo nzima bado, mimi ni mwanamke yule aliyesimama humu Nyumbani pamoja na wewe kumlalamikia Bwana. Nalimlalamikia kwa ajili ya mtoto huyu, Bwana akanipa maombo yangu, niliyomwomba. Mimi nami ninamtoa na kumpa Bwana, awe wake siku zote, atakazokuwapo, kwani ameombwa kwake Bwana. Kisha wakamtambikia Bwana huko. Hana akaomba na kusema: Moyo wangu unashangilia kwa kuwa naye Bwana, pembe yangu imetukuka kwa nguvu za Bwana, nimeasama kinywa changu, kiwatishe wachukivu wangu, kwani ninaufurahia msaada wako. Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana, kwani pasipo wewe hakuna Mungu, wala hakuna mwamba kama Mungu wetu. Msizidi kusema makuu ya kujikuza, maneno makorofi yasitoke vinywani mwenu! Kwani Bwana ni Mungu mwenye ujuzi, kwake yeye hujaribiwa matendo ya watu. Pindi za mafundi wa vita huvunjika, lakini waliokwazwa hujivika nguvu. Walioshiba hufanya kazi, wapate chakula tu, lakini waliokuwa wenye njaa, njaa zao hukoma kabisa, mwanamke mgumba huzaa watoto saba, naye mwenye wana wengi hufifia. Bwana huua, naye hurudisha uzimani, yeye hushusha kuzimuni, tena hupaza juu. Bwana wengine huwakosesha mali, wengine huwazidishia, hunyenyekeza, tena hukuza; mnyonge humwinua uvumbini, mkiwa humtoa jaani, awaketishe pamoja nao walio wakuu akiwapa kiti chenye utukufu, kiwe chao, kwani misingi ya nchi ni yake Bwana, juu yao ameuweka ulimwengu. Huiangalia miguu yao wamchao, lakini wasiomcha huangamizwa penye giza, kwa kuwa hakuna mtu atakayeshinda kwa nguvu zake. Watakaoshindana na Bwana watapondwa, atakapovumisha ngurumo juu yao mbinguni. Bwana atayahukumu mapeo ya nchi, naye mfalme wake atampa uwezo atakapoitukuza pembe yake yeye, aliyempaka mafuta. Kisha Elkana akaenda Rama nyumbani kwake, lakini yule mtoto akawa akimtumikia Bwana machoni pake mtambikaji Eli. Wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kabisa, hawakumjua Bwana, wala haki za watambikaji, wala haki za watu: mtu ye yote alipotoa ng'ombe ya tambiko, nyama zilipotokota, mtumishi wa mtambikaji huja akishika mkononi uma mkubwa wenye michomo mitatu, akakoroga nao chunguni au kaangoni au sufuriani au bakulini, nazo nyama zote, ule uma ulizozipandisha, mtambikaji huzichukua. Ndivyo, walivyowafanyizia Waisiraeli wote, wakija huko Silo. Napo, walipokuwa hawajachoma mafuta, mtumishi wa mtambikaji huja, amwambie mwenye kutambika: Nipe nyama ya kumchomea mtambikaji! Naye hataki kwako nyama iliyopikwa, ila mbichi. Yule mtu akimwambia: Leo watayachoma mafuta, kisha jichukulie, roho yako iyatakayo, humwambia: Sharti unipe sasa hivi! Kama hutaki, nitachukua kwa nguvu. Kwa hiyo ukosaji wao hao vijana ukawa mkubwa sana machoni pake Bwana, kwani kwa hiyo watu wakavibeza vipaji vya tambiko, Bwana alivyotolewa. Lakini mtoto Samweli akamtumikia Bwana, akawa amevikwa kisibau cha mtambikaji cha nguo ya ukonge. Naye mama yake akamshonea kanzu ndogo, akampelekea mwaka kwa mwaka, alipopanda na mumewe kutoa ng'ombe ya tambiko ya mwaka. Eli akambariki Elkana na mkewe akisema: Bwana na akupatie kizazi kwake mwanamke huyu cha kumlipa ombo lake, alilomwomba Bwana! Kisha wakaenda zao kufika kwao. Naye Bwana akamkagua Hana, akapata mimba, akazaa watoto wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye mtoto Samweli akawako akikua machoni pake Bwana. Eli akawa mkongwe kabisa; alipoyasikia yote, wanawe wanayowafanyizia Waisiraeli wote, tena ya kuwa hulala na wanawake wanaotumikia langoni penye Hema la Mkutano, akawaambia: Mbona mnafanya mambo mabaya kama hayo, mimi ninayoyasikia na hawa watu wote, ya kuwa mnayafanya? Msifanye hivyo wanangu! Kwani uvumi huu, ninaousikia mimi wa kuwakosesha watu wa Bwana, si mwema. Mtu akimkosea mtu mwenziwe, Mungu atampatiliza, lakini akimkosea Bwana, yuko nani atakayemwombea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwani Bwana alitaka kuwaua. Lakini mtoto Samweli akaendelea kukua na kuwa mwema machoni pake Bwana, napo machoni pa watu. Kisha mtu wa Mungu akaja kwa Eli, akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kumbe sikujitokeza kwa mlango wa baba yako, walipoutumikia mlango wa Farao huko Misri? Nikauchagua katika mashina yote ya Waisiraeli kuwa watambikaji, wapande pangu pa kutambikia na kuvukiza uvumba na kuvaa kisibau cha mtambikaji mbele yangu, nikaupa mlango wa baba yako ng'ombe zote za tambiko, wana wa Isiraeli wanazozitoa za kuteketezwa motoni. Mbona mnazipiga mateke ng'ombe zangu za tambiko na vipaji vyangu vya tambiko, nilivyoagiza, wavitoe katika Kao langu? Unawacha wanao kuliko mimi, mpate kujinonesha na kuvila vipande vilivyo vizuri vya vipaji vyote vya tambiko vyao walio ukoo wangu wa Isiraeli. Kwa hiyo ndivyo, asemavyo Bwana Mungu wa Isiraeli: Kweli nilisema, mlango wako na mlango wa baba yako na waendelee machoni pangu kale na kale. Lakini sasa ndivyo, asemavyo Bwana: Hili na liniendee mbali! Kwani anichaye nitampa macheo, lakini anibezaye atabezwa naye. Utaona, siku zikija, nitakapoukata mkono wako nayo mikono yao walio wa mlango wa baba yako, asipatikane mzee katika mlango wako. Ndipo, utakapoutazama ukiwa wa kao lako ukiona mema yote, atakayowafanyizia Waisiraeli, kwani siku hizo zote hatakuwapo mzee katika mlango wako. Ijapo nisimwangamize ye yote wa kwako na kumtoa pangu pa kutambikia, atakuwa tu wa kuyafifiliza macho yako na wa kuikatisha roho yako tamaa, lakini wao wengi wa mlango wako watakufa watakapokuwa waume wazima. Kielekezo chako yatakuwa hayo yatakayowapata wanao wawili Hofuni na Pinehasi: hao wawili watakufa siku moja. kisha nitajiinulia mtambikaji mwelekevu atakayeyafanya mapenzi ya moyo wangu na ya Roho yangu; yeye nitamjengea nyumba ya kweli, aendelee siku zote machoni pake yule, nitakayempaka mafuta. Nao wote watakaosazwa katika mlango wako watamjia na kumwangukia, wapate thumuni tu au mkate mdogo na kumwomba: Nipe kazi moja tu ya utambikaji, nipate kula kipande cha mkate! Mtoto Samweli alipomtumikia Bwana machoni pa Eli, Neno la Bwana lilimkalia mmojammoja tu, hayakuwako maono ya wachunguzaji yaliyoenea po pote. Ikawa siku zile, Eli alikuwa amelala mahali pake, nayo macho yalikuwa yameanza kuguiwa na giza, asiweze kuona vema. Nayo taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, naye Samweli alikuwa amelala Jumbani mwa Bwana, Sanduku la Mungu lilimokuwa. Ndipo, Bwana alipomwita Samweli, naye akaitikia: Mimi hapa! Akamtokea Eli upesi, akamwambia: Mimi hapa! kwani umeniita. Akajibu: Sikukuita, rudi, ulale! Akaenda zake, akalala. Bwana akaita tena mara ya pili: Samweli! Samweli akaamka, akaja kwake Eli na kumwambia: Mimi hapa! kwani umeniita. Akajibu: Sikukuita, mwanangu; rudi, ulale! Naye Samweli alikuwa hajamjua Bwana bado, nalo Neno la Bwana halijamtokea bado. Bwana akaendelea kuita mara ya tatu: Samweli! Akaamka, akaenda kwake Eli na kumwambia: Mimi hapa! kwani umeniita. Ndipo, Eli alipotambua, ya kuwa ni Bwana aliyemwita mtoto. Kisha Eli akamwambia Samweli: Nenda, ulale! Itakapokuwa, akuite tena, itikia kwamba: Sema, Bwana! kwani mtumishi wako anasikia. Samweli akaenda, akalala mahali pake. Bwana akaja, akasimama, akaita, kama alivyoita mara za kwanza: Samweli! Samweli! Samweli akaitikia: Sema! kwani mtumishi wako anasikia. Bwana akamwambia Samweli: Utaniona, nikifanya jambo kwao Waisiraeli, nao wote watakaolisikia masikio yao yote mawili yatawavuma. Siku hiyo nitamtimilizia Eli yote, niliyoyasema ya mlango wake, toka mwanzo hata mwisho. Kwani nimempasha habari, ya kuwa nitauhukumu mlango wake kale na kale kwa ajili ya manza, walizozikora; kwani alijua, ya kuwa wanawe wanajipatia kiapizo, lakini hakuwakaripia. Kwa hiyo nimeuapiza mlango wa Eli kwamba: Manza, walizozikora wao wa mlango wa Eli, hazitawezekana kale na kale kupatiwa upozi, wala kwa ng'ombe ya tambiko, wala kwa kipaji cha tambiko cho chote. Kisha Samweli akaja kulala, mpaka kuche, kisha akaifungua milango ya Nyumba ya Bwana; lakini Samweli akaogopa kumsimulia Eli, aliyoyaona. Eli akamwita Samweli, akasema: Mwanagu, Samweli! Akaitikia: Mimi hapa! Eli akamwuliza: Ni neno gani, alilokuambia? Usinifiche kamwe! Mungu na akufanyizie hivi na hivi, ukinificha neno moja tu la hayo maneno yote, aliyokuambia. Ndipo, Samweli alipomsimulia hayo maneno yote, hakumficha. Akajibu: Yeye ni Bwana, na ayafanye yaliyo mema machoni pake. Samweli akakua, Bwana akiwa pamoja naye; nayo maneno yake yote hakuna hata moja, aliloliangusha chini. Waisiraeli wote toka Dani hata Beri-Seba wakatambua, ya kuwa Samweli amekwisha kuelekezwa kuwa mfumbuaji wa Bwana. Bwana akaendelea kuonekana huko Silo, kwani Bwana alimtokea Samweli huko Silo, kama Bwana alivyosema; kisha neno la Samweli likawajia Waisiraeli wote. Waisiraeli wakatoka kupigana na Wafilisti, wakapiga makambi huko Ebeni-Ezeri; nao Wafilisti wakapiga makambi Afeki. Kisha Wafilisti wakajipanga kuwaelekea Waisiraeli; mapigano yalipoenea pakubwa, Waisiraeli wakapigwa na Wafilisti, hao wakaua watu kama 4000 papo hapo porini, walipojipanga kupigana. Watu walipokuja kuingia makambini, wazee wa Waisiraeli wakasema: Sababu gani Bwana ametupiga leo machoni pao Wafilisti? Na tulichukue huko Silo Sanduku la Agano la Bwana, lije lituokoe mikononi mwa adui zetu. Ndipo, watu walipotuma Silo, wakalichukua huko Sanduku la Agano la Bwana Mwenye vikosi akaaye juu ya Makerubi; nao wale wana wawili wa Eli, Hofuni na Pinehasi, wakatoka huko wakilisimamia Sanduku la Agano la Mungu. Ikawa, Sanduku la Agano la Bwana lilipoingia makambini, Waisiraeli wote wakapaza sauti sana na kupiga yowe, hata nchi ikatutuma. Wafilisti walipozisikia sauti zao za yowe wakaulizana: Sauti hizi kuu za yowe makambini mwa Waebureo ni za nini? Wakatambua, ya kuwa Sanduku la Bwana limeingia makambini. Wafilisti wakashikwa na woga, kwani walisema: Mungu ameingia makambini! Yametupata sasa! Kwani jambo kama hilo halijafanyika zamani zote. Yametupata sasa! Yuko nani atakayetuponya mkononi mwake Mungu huyu mwenye nguvu? Huyu ni Mungu yule aliyewapiga Wamisri mapigo yote nyikani. Lakini ninyi Wafilisti jipeni mioyo, mwe waume, msije kuwatumikia Waebureo, kama wao wanavyowatumikia ninyi. Mwe waume, mje kupigana nao! Basi, Wafilisti walipopigana nao, Waisiraeli wakapigwa, wakakimbilia kwao kila mtu hemani kwake; likawa pigo kubwa sana, kwao Waisiraeli wakauawa 30000 waliokwenda kwa miguu. Hata Sanduku la Mungu likatekwa, nao wale wana wawili wa Eli, Hofuni na Pinehasi, wakafa. Mtu wa Benyamini akatoka hapo, walipojipanga kupigana, akapiga mbio kufika Silo siku ileile; nguo zake zilikuwa zimerarukararuka, napo juu kichwani pake palikuwa na mavumbi. Alipofika akamwona Eli, akikaa langoni katika kiti chake cha ukuu kando ya njia na kuchungulia njiani, kwani moyo wake ulikuwa umehangaika kwa ajili ya Sanduku la Mungu. Yule mtu alipoingia mjini kupasha habari, watu wote wa mjini wakalia. Eli alipozisikia sauti za kilio akauliza: Sauti hizi za huo mtutumo ni za nini? Ndipo, yule mtu alipopiga mbio kufika kwake na kumpasha Eli hizo habari. Naye Eli alikuwa mwenye miaka 98, macho yake yalikuwa yametenda kiwi, asiweze kuona. Yule mtu akamwambia Eli: Mimi nimetoka hapo, walipojipanga kupigana; nami nimekimbia leo hivi kutoka hapo, walipojipanga kupigana. Akauliza: Mambo ya huko yako namna gani, mwanangu? Mwenye kuleta habari akajibu na kusema: Waisiraeli wamekimbizwa na Wafilisti, likawa pigo kubwa sana kwao, nao wanao wawili, Hofuni na Pinehasi, wamekufa, hata Sanduku la Mungu limetekwa. Ikawa, alipolitaja Sanduku la Mungu, ndipo, Eli alipoanguka chali hapo kitini kando ya lango, shingo lake likavunjika, akafa, kwani alikuwa mzee na mtu mnene sana. Nayo miaka, aliyokuwa mwamuzi wa Waisiraeli, ilikuwa 40. Mkwewe, mkewe Pinehasi, alikuwa mwenye mimba iliyokomaa; alipopashwa hizo habari za kutekwa kwake Sanduku la Mungu nazo za kufa kwake mkwewe na mumewe, akaanguka magotini, akazaa, kwani alishikwa na uchungu wake wa kuzaa. Hapo, alipotaka kufa, wanawake waliomsimamia wakamwambia: Usiogope! Kwani umezaa mtoto wa kiume; lakini hakujibu neno, wala hakusikiliza. Lakini mtoto akamwita jina lake Ikabodi ni kwamba: Utukufu umeondoka kwao Waisiraeli, kwa kuwa Sanduku la Mungu lilikuwa limetekwa, nao mkwewe na mumewe walikuwa wamekufa. Akasema: Utukufu umeondoka kwao Waisiraeli, kwani Sanduku la Mungu limetekwa. Wafilisti wakalichukua Sanduku la Mungu, wakalitoa Ebeni-Ezeri, wakalipeleka Asdodi. Wafilisti walipolichukua Sanduku la Mungu wakaliingiza nyumbani mwa Dagoni, wakaliweka kando yake Dagoni. Kesho yake watu wa Asdodi walipoamka asubuhi wakamkuta Dagoni, akilala usoni chini mbele ya Sanduku la Bwana; wakamchukua Dagoni, wakamrudisha mahali pake. Kesho yake walipoamka asubuhi wakamkuta Dagoni tena, akilala usoni chini mbele ya Sanduku la Bwana, nacho kichwa cha Dagoni na viganja vyote viwili vya mikono yake vilikuwa vimekatika, vilikuwa penye kizingiti, nao mwili ulikuwa umesalia peke yake. Kwa hiyo watambikaji wa Dagoni nao wote wanaoingia nyumbani mwa Dagoni hawakikanyagi kizingiti cha Dagoni huko Asdodi mpaka siku hii ya leo. Mkono wa Bwana ukawalemea watu wa Asdodi, akawaangamiza na kuwapiga kwa majipu mabaya waliokuwamo Asdodi namo katika mipaka yake. Watu wa Asdodi walipoyaona mambo hayo kuwa hivyo wakasema: Sanduku la Mungu wa Waisiraeli halitakaa tena kwetu, kwani mkono wake umetulemea sisi na mungu wetu Dagoni. Wakatuma, wakawakusanya wakuu wote wa Wafilisti kwao, wakauliza: Tulifanyie nini Sanduku la Mungu wa Waisiraeli? Wakasema: Sanduku la Mungu wa Waisiraeli na lihamishwe Gati! Wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Waisiraeli. Ikawa, walipokwisha kulihamisha, ndipo, mkono wa Bwana ulipoustusha mji huo, likawa stusho kubwa sana, akiwapiga watu wa mji huo, wakubwa kwa wadogo, wakatoka majipu mabaya. Ndipo, walipolipeleka Sanduku la Mungu Ekroni; ikawa, Sanduku la Mungu lilipoingia Ekroni, watu wa Ekroni wakalia kwamba: Sanduku la Mungu wa Waisiraeli wamelihamisha kwetu, wawaue watu wa kwetu. Ndipo, walipotuma, wakawakusanya wakuu wote wa Wafilisti, wakasema: Lipelekeni Sanduku la Mungu wa Waisiraeli, lirudi mahali pake, lisituue sisi na watu wa kwetu! Kwani katika mji wote mzima walishikwa na kistusho cha kifo, kwani mkono wa Mungu uliwalemea sana huko. Nao watu wasiokufa wakapigwa kwa majipu mabaya, vilio vya humo mjini vikafika mbinguni juu. Sanduku la Bwana lilipokuwa miezi saba katika nchi ya Wafilisti, Wafilisti wakawaita watambikaji na waaguaji na kuwauliza: Sanduku la Bwana tulifanyie nini? Tujulisheni njia ya kulipeleka mahali pake! Wakajibu: Mkilipeleka Sanduku la Mungu wa Waisiraeli, msilipeleke bure tu, ila sharti mlirudishe pamoja na kipaji cha tambiko cha upozi. Ndipo, mtakapopona, tena itajulikana kwenu, kama ni kwa sababu gani, mkono wake usipoondoka kwenu. Wakauliza: Kipaji cha tambiko cha upozi, tutakachomtolea tukilirudisha, ndio nini? Wakajibu: Kwa hesabu ya wakuu wa Wafilisti mifano mitano ya dhahabu ya hayo majipu mabaya, tena mifano mitano ya dhahabu ya panya. Kwani pigo lililowapata watu wote nanyi wakuu ni lilelile moja. Ifanyeni hiyo mifano ya majipu yenu mabaya na ya panya wenu wanaoiangamiza nchi hii, kisha mmpe Mungu wa Waisiraeli macheo, labda ataugeuza mkono wake kuwa mwepesi kwenu na kwa miungu yenu na katika nchi yenu. Mbona mnaishupaza mioyo yenu, kama Wamisri na Farao walivyoishupaza mioyo yao? Je sivyo? Alipowafanyia mabaya, wakawapa ruhusa, waende zao? Sasa tengenezeni gari jipya moja, tena chukueni ng'ombe wawili wanyonyeshao, wasiobandikiwa bado mti wa kuvutia gari! Kisha wafungeni hao ng'ombe penye hilo gari, miwaondoa watoto wao kwao na kuwarudisha nyumbani. Kisha lichukueni Sanduku la Bwana, mliweke garini pamoja na vile vyombo vya dhahabu, mtakavyomlipa kuwa kipaji cha tambiko cha upozi. Hivyo vitieni katika kisanduku kando yake, kisha lipelekeni, liende kwao! Kisha tazameni: likishika njia ya kuupandia mpaka wa Beti-Semesi, basi, ndilo lililotupatia haya mabaya makubwa mno; lakini kama sivyo, ndipo, mtakapojua, ya kuwa sio mkono wake uliotupiga, ila ni tukio tu lililotupata. Nao watu wakafanya hivyo, wakachukua ng'ombe wawili wanyonyeshao, wakawafunga penye gari, nao watoto wao wakawafungia nyumbani. Kisha wakaliweka Sanduku la Bwana garini pamoja na kisanduku chenye panya za dhahabu na mifano ya majipu yao mabaya. Ndipo, ng'ombe waliposhika njia ya kwenda moja kwa moja, ndio njia ya Beti-Semesi; wakaenda wakilia na kuifuata barabara hiyo moja tu, hawakuiacha kwenda kuumeni wala kushotoni. Nao wakuu wa Wafilisti wakawafuata hata mpakani kwa Beti-Semesi. Nao watu wa Beti-Semesi walikuwa wakivuna ngano bondeni; walipoyainua macho yao wakaliona hilo Sanduku, wakafurahi kuliona. Lile gari likaingia shambani kwa Yosua wa Beti-Semesi, likasimama huko, nako huko kulikuwa na jiwe kubwa. Basi, wakaipasua miti ya gari, nao hao ng'ombe wakamtolea Bwana kuwa ng'ombe za tambiko. Nao Walawi wakalishusha Sanduku la Bwana na kile kisanduku kilichowekwa pamoja nalo, kilichotiwa vile vyombo vya dhahabu, wakaliweka juu ya hilo jiwe kubwa. Kisha watu wa Beti-Semesi wakatoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, wakachinja nazo ng'ombe nyingine za tambiko siku ileile. Wale wakuu watano wa Wafilisti walipokwisha kuviona wakarudi Ekroni siku ileile. Nayo mifano ya dhahabu ya majipu, Wafilisti waliyoilipa, iwe kipaji cha tambiko cha upozi, ni hii: mmoja wa Asdodi, mmoja wa Gaza, mmoja wa Askaloni, mmoja wa Gati, mmoja wa Ekroni. Nazo panya za dhahabu hesabu yao ilikuwa sawa na hesabu ya miji yote ya Wafilisti ya hao wakuu watano, ya miji yenye maboma na ya vijiji vya shambani. Hivi vinashuhudiwa na lile jiwe kubwa, ambalo wameliweka Sanduku la Bwana juu yake, nalo liko hata siku hii ya leo shambani kwa Yosua huko Beti-Semesi. (Bwana) akawapiga watu wa Beti-Semesi, kwa kuwa wamechungulia Sandukuni mwa Bwana, akapiga kwao watu 70, tena watu 50000; ndipo, watu walipolia sana, kwa kuwa Bwana amewapiga wa kwao pigo kubwa. Watu wa Beti-Semesi wakasema: Yuko nani awezaye kusimama mbele ya Bwana, huyu Mungu mtakatifu? Sasa aende kwa nani akitoka kwetu? Wakatuma wajumbe kwa wenyeji wa Kiriati-Yearimu kwamba: Wafilisti wamelirudisha Sanduku la Bwana; haya! Telemkeni, mlipandishe kwenu! Watu wa Kiriati-Yearimu wakaja, wakalichukua Sanduku la Bwana kwao, wakaliingiza nyumbani mwa Abinadabu kilimani juu, naye mwanawe Elazari wakamweua, aliangalie Sanduku la Bwana. Tangu siku hiyo, Sanduku la Bwana lilipokuja kukaa Kiriati-Yearimu, siku zikapita nyingi, zikawa miaka 20. Kisha mlango wote wa Waisiraeli wakageuka kumfuata Bwana na kumlilia. Ndipo, Samweli alipouambia mlango wote wa Waisiraeli kwamba: Ninyi mkimgeukia Bwana kwa mioyo yote, iondoeni miungu migeni kwenu pamoja na Maastaroti! Kisha ielekezeni mioyo yenu kwake Bwana na kumtumikia yeye peke yake! Ndivyo, atakavyowaponya mikononi mwa wafilisti. Ndipo, wana wa Isiraeli walipoyaondoa Mabaali na Maastaroti, wakamtumikia Bwana peke yake. Kisha Samweli akasema: Wakusanyeni Waisiraeli wote Misipa, niwaombee kwake Bwana! Wakakusanyika Misipa, wakachota maji, wakayamwaga mbele ya Bwana na kufunga mfungo siku hiyo na kusema huko: Tumemkosea Bwana! Kisha Samweli akawakatia wana wa Isiraeli mashauri huko Misipa. Wafilisti waliposikia, ya kuwa wana wa Isiraeli wamekusanyika Misipa, wakuu wa Wafilisti wakawapandia Waisiraeli; nao Waisiraeli walipovisikia, wakawaogopa Wafilisti. Ndipo, wana wa Isiraeli walipomwambia Samweli: Usikome kumlilia Bwana Mungu wetu kwa ajili yetu, atuokoe mikononi mwa Wafilisti! Samweli akachukua mwana kondoo mwenye kunyonya, akamatolea Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima; samweli alipomlilia Bwana hivyo kwa ajili ya Waisiraeli, Bwana akamwitikia. Ikawa, Samweli alipoiteketeza hiyo ng'ombe ya tambiko, Wafilisti wakafika kupigana nao Waisiraeli. Papo hapo Bwana akanguruma kwa sauti kubwa sana juu ya Wafilisti; ndivyo, alivyowastusha sana, kwa hiyo wakapigwa mbele yao Waisiraeli. Kisha waume wa Waisiraeli wakatoka Misipa, wakawakimbiza na kuwapiga hata chini ya Beti-Kari. Ndipo, Samweli alipotwaa jiwe moja, akalisimika katikati ya Misipa na Seni, akaliita jina lake Ebeni-Ezeri (Jiwe la Msaada) akisema: Bwana ametusaidia mpaka hapa. Ndivyo, Wafilisti walivyonyenyekezwa, hawakurudi tena kuingia katika mipaka ya Waisiraeli, nao mkono wa Bwana ukawapinga Wafilisti siku zote za Samweli. Nayo miji, Wafilisti waliyoichukua kwa Waisiraeli, ikarudi tena kuwa yao Waisiraeli toka Ekroni hata Gati, nazo nchi zao Waisiraeli wakaziponya mikononi mwa Wafilisti. Tena Waisiraeli na Waamori walikuwa wakipatana. Naye Samweli akawa mwamuzi wa Waisiraeli siku zote za maisha yake. Mwaka kwa mwaka akaenda kuzunguka Beteli na Gilgali na Misipa, akikata mashauri yao Waisiraeli mahali hapo pote. Kisha hurudi Rama, kwani ndiko, nyumba yake ilikokuwa, tena ndiko, alikowaamulia Waisiraeli. Kisha akajenga huko pa kumtambikia Bwana. Ikawa, Samweli alipokuwa mzee, akawaweka wanawe wawili kuwa waamuzi wa Waisiraeli. Jina la mwanawe wa kwanza ni Yoeli, nalo lake wa pili ni Abia, nao walikaa Beri-Seba, walipokuwa waamuzi. Lakini wanawe hawakuendelea na kuzishika njia zake, maana waligeukia kutafuta mali, kwa hiyo wakachukua fedha za kupenyezewa, wakayapotoa mashauri. Ndipo, wazee wote wa Waisiraeli walipokusanyika, wakaja Rama kwa Samweli, wakamwambia: Tazama! Wewe umekwisha kuwa mzee, nao wanao hawaendelei na kuzishika njia zako, sasa tuwekee mfalme wa kutuamulia, kama mataifa yote yanavyoamuliwa! Neno hili likawa baya machoni pake Samweli, kwa kuwa wamesema: Tupe mfalme wa kutuamulia! Kwa hiyo Samweli akamwomba Bwana. Bwana akamwambia Samweli: Viitikie vinywa vyao watu hawa ukiyafanya yote, waliyokuambia! Kwani hawakukatai wewe, ila ni mimi, waliyenikataa kuwa mfalme wao. Ndivyo, matendo yao yote yalivyo, waliyoyatenda tangu siku ile, nilipowatoa Misri, mpaka siku hii ya leo wakiniacha na kutumikia miungu mingine. Hivi ndivyo, wanavyokufanyia hata wewe. Sasa viitikie vinywa vyao! Lakini sharti uwashuhudie vema na kuieleza haki yake mfalme atakayewatawala. Kisha Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme haya maneno yote ya Bwana akisema: Hii ndiyo haki yake mfalme atakayewatawala: atawachukua wana wenu wa kiume, awaweke katika magari yake wa kuyaendesha, wengine atawapandisha farasi, wengine atawaweka kuyatangulia magari yake kwa kupiga mbio. Wengine atawaweka kuwa wakuu wa maelfu na wakuu wa hamsini tu; wengine atawaweka kuyalima mashamba yake na kuyavuna mavuno yake na kuyatengeneza mata ya vita vyake na vyombo vya magari yake. Nao wana wenu wa kike atawachukua, wawe watengeneza manukato na wapishi na waoka mikate. Nayo mashamba na mizabibu na michekele yenu iliyo mizuri zaidi ataichukua na kuwapa watumishi wake. Tena mbegu zenu na mizabibu yenu atatoza mafungu ya kumi, awape watumishi wake wa nyumbani na watumishi wake wengine. Nao watumishi wenu wa kiume na wa kike na vijana wenu walio wazuri zaidi na punda wenu atachukua, awatumie katika kazi zake. Mbuzi na kondoo wenu atatoza mafungu ya kumi, nanyi sharti mmtumikie kitumwa. Tena siku hiyo, mtakapolia kwa ajili ya mfalme wenu, mliyejichagulia, siku hiyo Bwana hatawajibu. Lakini watu wakakataa kukiitikia kinywa cha Samweli, wakasema: Haidhuru, sharti tuwe na mfalme wa kututawala! Nasi tunataka kuwa kama mataifa yote, mfalme wetu atukatie mashauri yetu, tena atutangulie, avipige vita vyetu. Samweli alipokwisha kuyasikia maneno yote ya watu, akaja kuyasema masikioni mwa Bwana. Bwana akamwambia Samweli: Viitikie vinywa vyao na kuwapatia mfalme! Ndipo, Samweli alipowaambia waume wa Waisiraeli: Nendeni zenu kila mtu mjini kwake! Kulikuwa na mtu wa Benyamini, jina lake Kisi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorati, mwana wa Afia, mwana wa mtu wa Benyamini, naye alikuwa fundi wa vita mwenye nguvu. Alikuwa na mwana wa kiume, jina lake Sauli, naye alikuwa kijana mzuri mno, kwa Waisireli hakuwako mtu mzuri zaidi kuliko yeye, naye aliwapita watu wote kwa urefu wa kichwa kimoja, kikianza kupimwa mabegani. Punda wa kike wa Kisi, babake Sauli, walipopotea, Kisi akamwambia mwanawe Sauli: Chukua mmoja wao vijana, uondoke kwenda kuwatafuta hao punda! Basi, akapitia milimani kwa Efuraimu, kisha akapitia hata katika nchi ya Salisa, lakini hakuwaona. Kisha akapitia katika nchi ya Saalimu, nako walikuwa hawako. Kisha akapitia katika nchi ya Benyamini, lakini hawakuwaona. Kisha wakaingia katika nchi ya Sufu; ndipo, Sauli alipomwambia yule kijana, aliyekuwa naye: Haya! Na turudi, baba asiwaache wale punda, akatuhangaikia sisi. Naye akamwambia: Tazama! Humu mjini yumo mtu wa Mungu, naye ni mwenye macheo, kwani yote, anayoyasema, hutimia; sasa twende huko, labda atatuonyesha njia, tutakayoishika. Sauli akamwambia huyo kijana wake: Tazama! Tukienda, tutampelekea nini yule mtu? Kwani pamba zetu zimekwisha katika vyombo vyetu, hata tunzo hatunalo la kumpelekea yule mtu wa Mungu. Kiko nini, tulicho hacho? Yule kijana akamjibu Sauli tena akisema: Tazama, mkononi mwangu imeonekana thumuni! Hii nitampa yule mtu wa Mungu, atuonyeshe njia yetu. Hapo kale kwao Waisiraeli mtu alipokwenda kumwuliza Mungu husema: Haya! Twende kwa mtazamaji! Kwani mfumbuaji wa leo kale huitwa mtazamaji. Sauli akamwambia kijana wake: Neno lako ni jema; haya! Twende! Wakaja mle mjini, yule mtu wa Mungu alimokuwa. Wao walipokwea hapo pa kupandia kwenda mjini wakaona vijana wa kike waliotoka kuchota maji, wakawauliza hao: Mtazamaji yuko wapi humu? Wakawajibu na kuwaambia: Tazama, yuko mbele yako! Piga mbio sana! Kwani ameingia leo humu mjini, kwa kuwa leo watu wanatambika huko kilimani pa kutambikia. Mtakapoingia mjini, mtamkuta, hajapanda kilimani kula, kwani watu hawali, mpaka aje, kwani yeye kwanza sharti aibariki ng'ombe ya tambiko, kisha waalikwao hula. Sasa pandeni! Kwani siku kama hii ya leo mtamwona. Walipopanda mjini na kuingia humo mjini kati, mara Samweli akatokea, akakutana nao akitaka kupanda kilimani pa kutambikia. Nayo siku hiyo iliyotangulia kufika kwake Sauli Bwana alikuwa amemfumbulia Samweli masikioni mwake kwamba: Kesho wakati huu nitatuma kwako mtu wa nchi ya Benyamini; yeye ndiye, utakayempaka mafuta, awe mkuu wao walio ukoo wangu wa Waisiraeli. Naye ndiye atakayewaokoa walio ukoo wangu mikononi mwa Wafilisti, kwani nimewaona walio ukoo wangu, navyo vilio vyao vimefika kwangu. Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia: Tazama, yule mtu, niliyekuambia, anakuja kwako! Yeye ndiye atayewatawala walio ukoo wangu. Sauli akamkaribia Samweli langoni katikati na kumwambia: Niambie, nyumba ya mtazamaji iliko! Samweli akamjibu Sauli kwamba: Mtazamaji ni mimi; unitangulie kwenda huko kilimani pa kutambikia! Leo mtakula pamoja nami, kesho nitakuaga nikiisha kukuambia yote yaliyomo moyoni mwako. Nao wale punda wa kike waliokupotelea leo siku ya tatu usiwahangaikie moyoni mwako! kwani wameonekana. Kumbe mema yote ya Waisiraeli siyo yako na ya mlango wote wa baba yako? Sauli akajibu kwamba: Mimi si mwana wa Benyamini, nalo silo shina lililo dogo kuliko mengine ya Waisiraeli? Nao ukoo wangu ni mdogo kuliko koo zote za shina la Benyamini, mbona unaniambia maneno kama hayo? Kisha Samweli akamchukua Sauli na kijana wake, akawapeleka chumbani, walimolia ng'ombe ya tambiko, akawaketisha juu kwao walioalikwa, nao walikuwa kama watu 30. Samweli akamwambia mpishi: Lete hicho kipande, nilichokupa na kukuambia: Kiweke kwako! Mpishi akachukua paja pamoja na nyama zilizoshikana nalo, akamwandalia Sauli. Samweli akamwambia Sauli: Tazama iliyosazwa! Jiandalie, ule! Kwani niliposema: Nimewaalika watu, umewekewa nyama hii kuwa ya saa hiihii. Basi, siku hiyo Sauli akala pamoja na Samweli. Kisha wakatelemka wakitoka kilimani pa kutambikia kwenda mjini, naye Samweli akaja kuongea na Sauli darini. Walipoamka asubuhi, mapambazuko yalipotokea, Samweli akamwita Sauli huko darini kwamba: Inuka, nikusindikize! Ndipo, Sauli alipoinuka, wakatoka wote wawili, yeye na Samweli, kwenda nje. Walipotelemka, wafike mwishoni kwa mji, Samweli akamwambia Sauli: Mwambie kijana huyu, apite kwenda mbele yetu! Alipopita kwenda mbele, akasema: Lakini wewe simama sasa, nikuambie neno la Mungu! Ndipo, Samweli alipokitwaa kichupa cha mafuta, akayamiminia kichwa chake, akamnonea midomo na kumwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyokupaka mafuta, uwe mkuu wao walio fungu lake. Utakapotoka kwangu leo, utaona watu wawili penye kaburi la Raheli mpakani mwa Benyamini huko Selsa, nao watakuambia: Wale punda wa kike, uliokwenda kuwatafuta, wameonekana. Tazama, baba yako ameyaacha mambo ya punda kwa kuwahangaikia ninyi akisema: Mwanangu nimfanyie nini? Utakapoondoka huko kwenda zako na kufika penye mvule wa Tabori, huko watu watatu watakutana na wewe, nao wanapanda kwenda Beteli kwa Mungu, mmoja anachukua wana mbuzi watatu, mmoja mikate mitatu, mmoja kiriba cha mvinyo. Nao watakuamkia na kukupa mikate miwili, nawe utaipokea mikononi mwao. Baadaye utafika kwenye kilima cha Mungu, ngome ya Wafilisti iliko. Utakapofika huko penye mji huo utakuta kikosi cha wafumbuaji wanaoshuka kilimani pa kutambikia wakitanguliwa na mapango na matoazi na mazomari na mazeze, nao wanakwenda wakifumbua maneno. Ndipo, roho ya Bwana itakapokujia, ufumbue pamoja nao; ndivyo, utakavyogeuzwa kuwa mtu mwingine. Hapo, hivyo vielekezo vitakapokutukia, fanya, mkono wako utakayoyaona! kwani Mungu yuko na wewe. Kisha shuka kunitangulia kwenda Gilgali! Nami utaniona, nikishuka kuja kwako kutoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na kuchinja ng'ombe za tambiko za shukrani. Utangoja siku saba, hata nitakapokuja kwako, nikujulishe utakayoyafanya. Ikawa, Sauli alipogeuka, atoke kwake Samweli, ndipo, Mungu alipougeuza moyo wake kuwa mwingine. Navyo vielekezo vile vyote vikatukia siku ile. Walipofika kule Gibea, wakaona kikosi cha wafumbuaji kilichokuja kukutana naye; ndipo, roho ya Mungu ilipomjia, naye akafumbua mambo katikati yao. Ikawa, wote waliomjua zamani zote walipomwona, ya kuwa anafumbua mambo pamoja na wafumbuaji, ndipo, watu hao waliposemezana kila mtu na mwenzake: Hivi vya mwana wa Kisi vinakuwaje? Kumbe Sauli naye yumo katika wafumbuaji? Mtu wa huko akajibu: Je? Baba yao ni nani? Kwa hiyo likawa fumbo la kwamba: Kumbe Sauli naye yumo katika wafumbuaji! Alipokwisha kufumbua mambo akaja kilimani pa kutambikia. Mjomba wake Sauli akamwuliza yeye na kijana wake: Mlikwenda wapi? Akajibu: Kuwatatufa wale punda wa kike; lakini tusipowaona tukaenda kwa Samweli. Mjomba wake Sauli akasema: Nisimulie, Samweli aliyowaambia! Sauli akamwambia mjomba wake: Ametupasha habari, ya kuwa wale punda wa kike wameonekana; lakini lile neno la ufalme, Samweli alilolisema, hakumsimulia. Kisha Samweli akawaita watu kuja kwake Bwana huko Misipa. Akawaambia wana wa Isiraeli: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli: Mimi niliwatoa Waisiraeli Misri, nikawaponya mikononi mwa Wamisri namo mikononi mwa wafalme wote waliowasumbua ninyi. Nanyi siku hii ya leo mmemkataa Mungu wenu aliyewaokoa katika mabaya na katika masongano yenu yote mkimwambia: Tuwekee mfalme, atutawale! Sasa jipangeni hapa machoni pake Bwana kwa mashina yenu na kwa maelfu yenu! Samweli alipokwisha kuyafikisha mashina yote, wakipiga kura, likashikwa shina la Benyamini. Kisha alipolifikisha shina la Benyamini milango kwa milango, ukashikwa mlango wa Matiri, kisha akashikwa Sauli, mwana wa Kisi. Lakini walipomtafuta hawakumwona. Ndipo, walipomwuliza Bwana tena: Mtu huyu amefika kweli huku? Bwana akajibu: Mtazameni, amejificha kwenye mizigo! Wakapiga mbio kwenda kumchukua huko. Alipokuja kusimama katikati ya watu aliwapita watu wote kwa urefu wa kichwa, kikianza kupimwa mabegani. Samweli akawaambia watu wote: Mmemwona, Bwana aliyemchagua? Kwani kwao watu wote hakuna afananaye naye. Ndipo, wote walipopiga yowe za kumshangilia kwamba: Pongezi, mfalme! Kisha Samweli akawaambia watu haki yake mfalme, akaiandika katika kitabu, akakiweka hapo pake Bwana; kisha Samweli akawaaga watu wote, waende zao kila mtu nyumbani kwake. Naye Sauli akaenda zake nyumbani kwake huko Gibea, nao vijana wenye nguvu, Mungu aliowahimiza mioyoni, wakamsindikiza. Lakini watu wasiofaa kitu wakasema: Huyu atatuokoaje? Wakambeza, hawakumletea matunzo. Lakini yeye akawa, kama hakuyasikia, waliyoyasema. Nahasi wa Waamoni akapanda, akapiga makambi huko Yabesi katika nchi ya Gileadi. Ndipo, watu wote wa Yabesi walipomwambia Nahasi: Fanya agano nasi, tukutumikie! Mwamoni Nahasi akawaambia: Basi, nitapatana nanyi hivyo: nitawachoma ninyi kila mtu jicho lake la kuume, niwatweze Waisiraeli wote. Wazee wa Yabesi wakamwambia: Tupe siku saba, tutume wajumbe kwenda katika mipaka yote ya Waisiraeli! Asipopatikana mwokozi wetu, tutakutokea. Wajumbe walipofika Gibea kwa Sauli na kuyasema maneno hayo masikioni pa watu, watu wote wakalia na kupaza sauti zao. Naye Sauli alikuwa anarudi malishoni akiwafuata ng'ombe; hapo Sauli akauliza: Watu wanalilia nini? Wakamsimulia habari, watu wa Yabesi walizozileta. Ndipo, roho ya Mungu ilipomjia Sauli, alipozisikia habari hizo, makali yake yakawaka moto. Akakamata ng'ombe wawili, akawakatakata, akawatuma wale wajumbe kwenda katika nchi zote za Waisiraeli na kuwapelekea watu vipande vya nyama kwamba: Kila mtu asiyetoka kumfuata Sauli na Samweli ng'ombe wake watafanyiziwa hivyo. Ndipo, watu walipoguiwa na kituko cha Bwana, wakatoka kama mtu mmoja. Alipowakagua huko Bezeki, wana wa Isiraeli walikuwa 300000, nao watu wa Yuda 30000. Wakawaambia wale wajumbe waliokuja: Hivi ndivyo, mtakavyowaambia watu wa Yabesi katika nchi ya Gileadi: Kesho, jua likianza kuwa kali, mtaona wokovu. Hao wajumbe waliporudi na kuwapasha habari hii, watu wa Yabesi wakafurahi. Nao watu wa Yabesi wakawaambia wale: Kesho tutawatokea, mtufanyizie yote yaliyo mema machoni penu. Kesho yake Sauli akawagawanya watu wake kuwa vikosi vitatu, wakaingia katikati ya makambi penye zamu ya kungoja, kuche, wakawapiga Waamoni, hata jua lilipokuwa kali mchana huo. Nao waliosalia wakatawanyika, wasisalie kwao wawili tu waliokuwa pamoja. Ndipo, watu walipomwambia Samweli: Wako wapi waliosema: Huyu Sauli awe mfalme wetu? Watoeni watu hawa, tuwaue! Lakini Sauli akasema: Asiuawe mtu wa kwetu siku hii ya leo! Kwani leo Bwana amewapatia Waisiraeli wokovu. Samweli akawaambia watu: Njoni, twende Gilgali, tuurudishie ufalme upya! Watu wote wakaja Gilgali, kisha wakamweka Sauli machoni pake Bwana huko Gilgali kuwa mfalme wao wakachinja huko machoni pake Bwana ng'ombe za tambiko za shukrani, naye Sauli akachangamka sanasana pamoja na Waisiraeli wote. Kisha Samweli akawaambia Waisiraeli wote: Tazameni! Nimeviitikia vinywa vyenu katika mambo yote, mliyoniambia, nikawapa hata mfalme wa kuwatawala. Sasa tazameni! Huyu mfalme huwatangulia, mimi nami nimekwisha kuwa mzee mwenye mvi, nao wanangu mnao kwenu, nami nimefanya mwenendo machoni penu tangu utoto wangu mpaka siku hii ya leo. Basi, nitazameni, mniumbue mbele ya Bwana na mbele ya mtu wake, aliyempaka mafuta, kama nimechukua ng'ombe wa mtu, au kama nimechukua punda wa mtu, au kama nimekorofisha mtu, au kama nimeponda mtu, au kama nimechukua mkononi mwa mtu fedha za kupenyezewa za kuyapofusha macho yangu! Kama ndivyo, nitawarudishia ninyi. Wakamwambia: Hukutukorofisha, wala hukutuponda, wala hukuchukua cho chote mkononi mwa mtu. Ndipo, alipowaambia: Siku hii ya leo Bwana ni shahidi wangu kwenu, naye aliyempaka mafuta ni shahidi wangu, ya kuwa hamkuona cho chote mkononi mwangu. Wakasema: Kweli, ndiye shahidi. Kisha Samweli akawaambia watu: Ni yeye Bwana aliyemwumba Mose naye Haroni, aliyewatoa baba zenu katika nchi ya Misri. Lakini sasa jipangeni, nisemezane nanyi usoni pake yeye Bwana kwa ajili ya wongofu wote, Bwana aliowatendea ninyi na baba zenu! Yakobo alipoingia Misri, baba zenu walipomlilia Bwana, Bwana akamtuma Mose na Haroni, akawatoa baba zenu huko Misri, akawakalisha mahali hapa. Walipomsahau Bwana Mungu wao, akawauza mkononi mwa Sisera, mkuu wa vikosi vya Hasori, namo mikononi mwa Wafilisti, namo mkononi mwa mfalme wa Moabu, walipowapelekea vita. Lakini walipomlilia Bwana na kusema: Tumekosa tukimwacha Bwana na kuyatumikia Mabaali na Maastaroti, sasa tuponye mikononi mwa adui zetu, tukutumikie, ndipo, Bwana alipomtuma Yerubaali na Bedani na Yefuta na Samweli, akawaponya mikononi mwa adui zenu waliowazunguka, mkapata kukaa na kutulia. Tena mlipoona, ya kuwa Nahasi, mfalme wa wana Amoni, anawajia, ndipo, mliponiambia: Hivi sivyo, sharti mfalme atutawale. Naye Mungu wenu alikuwa mfalme wenu. Sasa mfalme yuko, mliyemchagua kwa kumtaka; tazameni! Bwana amewapa naye mfalme wa kuwatawala. Kwa hiyo mcheni Bwana na kumtumikia na kuisikia sauti yake, msikikatae kinywa chake Bwana, ila mmfuate Bwana Mungu wenu, ninyi na mfalme anayewatawala! Lakini msipoisikia sauti ya Bwana na kukikataa kinywa chake Bwana, mkono wa Bwana utawapingia, kama ulivyowapingia baba zenu. Sasa simameni hapa, mlione jambo hili kubwa, Bwana atakalolifanya machoni penu! Je? Mavuno ya ngano hayakutimia? Leo hivi nitamwomba Bwana, alete ngurumo na mvua, mpate kutambua na kuona, ya kuwa hapo mlipojitakia mfalme mlifanya yaliyo mabaya sana machoni pake Bwana. Basi, Samweli alipomwomba Bwana, Bwana akaleta ngurumo na mvua siku hiyohiyo; ndipo, watu wote walipoingiwa na woga wa kumwogopa sana Bwana, hata Samweli. Kisha watu wote wakamwambia Samweli: Waombee watumishi wako kwake Bwana Mungu wako, tusife! Kwani makosa yetu yote tumeyaongeza na kibaya hiki cha kujitakia mfalme. Samweli akawaambia watu: Msiogope! Kweli ninyi mmeyafanya hayo mabaya yote, lakini msijiendee tena mkiacha kumfuata Bwana, ila mtumikieni Bwana kwa mioyo yenu yote! Msiondoke kwake na kufuata mambo ya ovyoovyo tu yasiyofaa, nayo hayaponyi kwa kuwa ya ovyoovyo tu. Kwani walio ukoo wake Bwana hatawatupa kwa ajili ya Jina lake kuu; kwani ndiye Bwana mwenyewe aliyewataka kuwa ukoo wake. Mimi nami hili na liniendee mbali, nisimkosee Bwana nikiacha kuwaombea! Ila nitawafundisha kuishika njia njema inyokayo. Ninyi mcheni tu Bwana na kumtumikia kweli kwa mioyo yenu yote, kwani mmeyaona makuu, Bwana aliyowafanyizia. Lakini mtakapofanya mabaya, mtaangamizwa ninyi na mfalme wenu. Sauli alipoupata ufalme alikuwa mwenye miaka (30); naye Sauli alipokuwa mfalme wa Waisiraeli miaka miwili, akajichagulia watu 3000 kwa Waisiraeli: 2000 wakawa naye Sauli huko Mikimasi na mlimani kwa Beteli, 1000 walikuwa na Yonatani huko Gibea wa Benyamini. Watu wengine akawapa ruhusa kwenda zao kila mtu hemani kwake. Yonatani akaipiga ngome ya Wafilisti iliyokuwa huko Geba, nao Wafilisti wakavisikia. Kisha Sauli akapiga baragumu katika nchi yote kwamba: Waebureo na wasikilize! Waisiraeli wote waliposikia ya kuwa Sauli ameipiga ngome ya Wafilisti, ya kuwa Waisiraeli wanawanukia Wafilisti vibaya, ndipo, watu wote walipokwitwa kumfuata Sauli kwenda Gilgali. Wafilisti nao wakakusanyika kupigana na Waisiraeli; magari 30000 na wapanda farasi 6000, nao watu wao wakawa wengi kama mchanga ulioko ufukoni kwenye bahari. Hao wakapanda, wakapiga makambi kule Mikimasi kuelekea Beti-Aweni, ni upande wake wa maawioni kwa jua. Watu wa Waisiraeli walipoona, ya kuwa wamesongeka kwa kukaribiwa na wale watu, wakajificha mapangoni na magengeni na miambani na mashimoni na makaburini. Waebureo wengine wakavuka Yordani kwenda katika nchi za Gadi na za Gileadi; lakini Sauli alikuwa yuko bado Gilgali, nao watu wote wakamfuata kwa kutetemeka tu. Alipongoja zile siku saba alizoagizwa na Samweli, naye Samweli asipokuja, watu wakatawanyika na kumwacha. Ndipo, Sauli aliposema: Nileteeni ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima na vipaji vya tambiko vya shukrani! Kisha akatambika na kuiteketeza hiyo ng'ombe ya tambiko. Ikawa, alipokwisha kuiteketeza hiyo ng'ombe ya tambiko, mara Samweli akaja, Sauli akatoka kumwendea njiani na kumpigia magoti. Samweli akamwuliza: Umefanya nini? Sauli akamwambia: Nimeona, ya kuwa watu wanatawanyika na kuniacha, wewe nawe hukuja siku hizo, tulizoagana, tena Wafilisti wamekwisha kukusanyika huko Mikimasi, basi, nikasema: Sasa Wafilisti watanishukia huku Gilgali, nikiwa sijamtokea Bwana na kumwomba, atuwie mpole; ndipo, nilipojipa moyo, nikatambika na kuiteketeza ng'ombe ya tambiko. Samweli akamwambia Sauli: Umefanya ujinga usipoliangalia agizo la Bwana Mungu wako, alilokuagiza, akapata sasa kuusimamisha ufalme wako wa kuwatawala Waisiraeli, uwe wa kale na kale. Lakini sasa ufalme wako hausimamiki, Bwana amekwisha kujitafutia mtu mwingine aupendezaye moyo wake, naye amemwagiza kuwa mkuu wao walio ukoo wake, kwani hukuyaangalia, Bwana aliyokuagiza. Kisha Samweli akaondoka na kutoka Gilgali, akaenda kupanda Gibea wa Benyamini. Naye Sauli akawakagua watu walioonekana kwake, wakawa kama watu 600. Sauli na mwanawe Yonatani na watu walioonekana kwao wakakaa katika Geba wa Benyamini, nao Wafilisti walikuwa wamepiga makambi yao Mikimasi. Kisha wenye kuangamiza wakatoka katika makambi ya Wafilisti, nao walikuwa vikosi vitatu; kimoja kikashika njia ya kwenda Ofura katika nchi ya Suali; kikosi cha pili kikashika njia ya Beti-Horoni, nacho kikosi cha tatu kikashika njia ya mpakani kunakoelekea Bonde la Mafisi upande wa nyikani. Katika nchi yote ya Waisiraeli hakuonekana mhunzi, kwani Wafilisti walisema: Waebureo wasijifanyie wala panga wala mikuki! Kwa hiyo Waisiraeli hawakuwa na budi kushuka kwao Wafilisti, kama mtu alitaka kunoa tu jembe lake au mundu wake au shoka lake au muo wake, makali ya majembe au ya miundu au ya pembe za uma au ya mashoka yakidugika, hata wakitaka tu kunyosha ncha za fimbo. Kwa hiyo siku ya mapigano hamkupatikana wala upanga wala mkuki mkononi mwa mtu kwao watu wote waliokuwa na Sauli na Yonatani, ila mata yakaonekana tu kwake Sauli na kwa mwanawe Yonatani. Kikosi cha Wafilisti kikatoka kwenda penye njia ya magemani huko Mikimasi. Siku moja Yonatani, mwanawe Sauli, akamwambia kijana aliyemchukulia mata yake: Njoo, twende, tuwashambulie wale Wafilisti wanaongoja zamu hapo ng'ambo! Lakini baba yake hakumwambia. Naye Sauli alikuwa akikaa kwenye mpaka wa Gibea chini ya mkomamanga ulioko Migroni, nao watu waliokuwa naye walikuwa kama 600 tu. Naye Ahia, mwana wa Ahitubu, ndugu ya Ikabodi, mwana wa Pinehasi, mwana wa Eli aliyekuwa mtambikaji wa Bwana huko Silo, ndiye aliyevaa kisibau cha mtambikaji. Hata watu hawakujua, ya kuwa Yonatani amekwenda zake. Napo magemani, Yonatani alipotafua njia ya kupitita, afike kwa Wafilisti waliongoja zamu hapo, palikuwa na jino la mwamba upande wa huku na jino jingie la mwamba upande wa huko, jina lake moja ni Bosesi, jina lake la pili Sene. Genge moja likasimama sawa upande wa kaskazini kuelekea Mikimasi, la pili upande wa kusini kuelekea Geba. Yonatani akamwambia kijana aliyemchukulia mata: Haya! Twende, tuwavumbukie hao wamizimu wasiotahiriwa wanaongoja zamu! Labda Bwana atatupigania, kwani Bwana hashindwi na kuokoa, ikiwa anatumia wengi au wachache. Mchukua mata yake akamwambia: Yafanye yote yaliyomo moyoni mwako! Jielekeze kwenda kwao! Tazama, niko pamoja na wewe po pote, moyo wako unapotaka. Yonatani akasema: Tazama! Tukipita kwenda kwao hao watu, tutaonwa nao. Itakapokuwa, watuambie: Simameni, mpaka tuwafikie karibu! tutasimama hapo chini, tusiwapandie; lakini itakapokuwa, watuambie: Tupandieni! basi, tutapanda, kwani Bwana amewatia mikononi mwetu. Hiki kitakuwa kielekezo chetu. Walipowaonekea Wafilisti waliongoja zamu, Wafilisti wakasema: Tazameni! Waebureo wametoka mashimoni, walimokuwa wamejificha. Wale watu wa zamu wakaanza kusema naye Yonatani na mchukua mata yake wakiwaambia: Tupandieni, tuwajulishe neno! Ndipo, Yonatani alipomwambia mchukua mata yake: Panda nyuma yangu! Kwani Bwana amewatia mikononi mwa Waisiraeli. Yonatani akapanda na kutumia mikono na miguu yake, naye mchukua mata yake nyuma yake. Kisha wakaangushwa na Yonatani, naye mchukua mata yake akamaliza kuwaua nyuma yake. Hivyo hili pigo la kwanza, alilolipiga Yonatani na mchukua mata yake, liliua watu kama 20, napo mahali pale palikuwa kama nusu tu ya shamba linalolimwa na ng'ombe wawili siku moja. Ndipo, watu wote walipostushwa waliokuwako makambini na mashambani, waliongoja zamu nao waliotembea kuangamiza tu, hao nao wakastushwa kweli, kwani hata nchi ilikuwa imetetemeka, wakawa wakimstukia Mungu. Nao walinzi wa Sauli waliokuwa huko Gibea wa Benyamini walikuwa wakichungulia, mara wakaona, huo mtutumo wa watu ulivyotoweka, wakienda huko na huko. Nipo, Sauli alipowaambia watu waliokuwa naye: Wakagueni watu, mwone, kama ni wa nani walioondoka kwetu. Walipowakagua watu wakaona, Yonatani na mchukua mata yake hawako. Kisha Sauli akamwambia Ahia: Lilete Sanduku la Mungu! Kwani Sanduku la Mungu lilikuwako siku hiyo kwao wana wa Isiraeli. Ikawa, Sauli aliposema na mtambikaji, makelele yaliyoko makambini kwa Wafilisti yakaendelea kuzidi sana; ndipo, Sauli alipomwamba mtambikaji: Urudishe mkono wako! Sauli na watu waliokuwa naye wakaitana; walipofika penye mapigano wakaona, ya kuwa wanapigana wao kwa wao kwa panga, kila mtu na mwenziwe, kukawa hangaiko kubwa sana. Kwani kwao Wafilisti kulikuwako Waebureo waliotekwa kale, nao walikuwa wamepanda nao kukaa makambini; nao waligeuka, wawe upande wa Waisiraeli pamoja na Sauli na Yonatani. Hata Waisiraeli wote waliojificha mlimani kwa Efuraimu waliposikia, ya kuwa Wafilisti wamekimbizwa, wakaja kuandamana nao wenye kuwafukuza Wafilisti vitani. Hivyo Bwana akawaokoa Waisiraeli siku hiyo; nayo mapigano yakaendelea kufika hata Beti-Aweni. Siku hiyo watu wa Waisiraeli wakachoka sana, lakini Sauli akawaapisha kwamba: Na aapizwe kila mtu atakayekula chakula mpaka jioni, nipate kuwalipiza adui zangu! Kwa hiyo hakuna mtu aliyeonja chakula Watu wote wa huko walipoingia mwituni, basi, kukawa na asali huko porini. Watu wote walipoingia mle mwituni, wakaona, asali inavyomwagika, lakini hakuwako mtu aliyeukunjua mkono wake kuipeleka kinywani mwake, kwani watu walikiogopa hicho kiapo. Lakini Yonatani hakusikia, baba yake alipowaapisha watu, kwa hiyo akaipeleka ncha ya fimbo yake, aliyoishika mkononi, akaichovya katika ute wa masega ya asali, akaurudisha mkono wake kinywani mwake; ndipo, macho yake yalipong'aa. Mtu mmoja akaanza kusema na kumwambia: Baba yako amewaapisha watu kwamba: Na aapizwe kila mtu atakayekula chakula leo! Watu walipotaka kuzimia, Yonatani akasema: Baba yangu anaiponza nchi hii. Nitazameni, macho yangu yanavyong'aa kwa kuwa nimeionja asali hii kidogo tu! Kama watu wangalikula leo nyara za adui zao, walizoziona, wangezidisha kazi, lakini sasa mapigo yao ya kuwapiga Wafilisti si mengi sana. Siku hiyo wakawapiga Wafilisti toka Mikimasi hata Ayaloni, kisha wakawa wenye kuzimia kabisa. Ndipo, watu walipozirukia hizo nyara, wakachukua mbuzi na kondoo na ng'ombe na ndama, wakawachinja papo hapo, nao watu wakawala pamoja na damu. Wengine walipompasha Sauli habari kwamba: Watu wanamkosea Bwana wakila nazo damu, akasema: Mwavunja maagano! Sasa hivi fingirisheni jiwe kubwa, lije huku kwangu! Kisha Sauli akaagiza: Tawanyikeni katika watu na kuwaambia, kila mtu alete ng'ombe wake na mbuzi au kondoo wake huku kwangu, mwachinje hapa! Kisha mtawala pasipo kumkosea Bwana kwa kula damu. Ndipo, watu wote walipopeleka usiku huo kwa mikono yao kila mtu ng'ombe wake, wakawachinja hapo. Naye Sauli akajenga pa kumtambikia Bwana; hii ndio mara ya kwanza akimjengea Bwana pa kumtambikia. Sauli akasema: Na tutelemke kuwafukuza Wafilisti na usiku, tupate kuteka mateka kwao, mpaka kuche, tusisaze kwao mtu hata mmoja! Watu wakasema: Yote yaliyo mema machoni pako yafanye! Lakini mtambikaji akasema: Kwanza tumkaribie Mungu hapa! Ndipo, Sauli alipomwuliza Mungu: Nitelemke kuwafukuza Wafilisti? Hukuwatia mikononi mwa Waisiraeli? Lakini siku hiyo hakumjibu. Ndipo, Sauli aliposema: Njoni hapa, ninyi wakuu wote mnaosimama pembeni kwa watu! Haya! Vumbueni, mwone, kama huku liko kosa gani lililofanyika leo! Hivyo, Bwana aliyewaokoa Waisiraeli alivyo Mwenye uzima, ijapo awe mwanangu Yonatani mwenyewe, hana budi kuuawa kabisa! Kwao watu wote hakuna aliyejibu. Kisha akawaambia Waisiraeli wote: Ninyi mwe upande mmoja, mimi nami na mwanagu Yonatani tuwe upande mmoja! Watu wakamwambia Sauli: Yaliyo mema machoni pako yafanye! Kisha Sauli akamwambia Bwana Mungu wa Isiraeli: Yaumbue yaliyokwisha kufanywa! Wakashikwa Yonatani na Sauli, nao watu wakapona. Sauli akasema: Nipigieni kura mimi na mwanangu Yonatani! Akashikwa Yonatani. Ndipo, Sauli alipomwambia Yonatani; Niambie! Umefanya nini? Yonatani akamsimulia kwamba: Nimeonja asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu, niliyoishika mkononi, sasa basi, nitakufa. Sauli akasema: Mungu na anifanyizie hivi na hivi, wewe Yonatani usipokufa kweli! Ndipo, watu walipomwambia Sauli: Je? Yonatani atakufa namna gani? Siye aliyewapatia Waisiraeli wokovu huu mkubwa? Hili na lituendee mbali! Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, unywele mmoja tu hautaanguka chini na kutoka kichwani pake! Ndivyo, watu walivyomwokoa Yonatani, asife. Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, akapanda kwenda zake; nao Wafilisti wakaenda zao kwao, walikokaa. Sauli alipoutwaa ufalme wa Waisiraeli akawapelekea vita adui zake wote waliokaa na kumzunguka: Wamoabu na wana wa Amoni na Waedomu na wafalme wa Soba na Wafilisti, napo pote, alipojielekezea, akawapatiliza vibaya. Hivyo akaendelea kupata nguvu, akawapiga Waamaleki, akawaponya Waisiraeli mwao waliowanyang'anya mali zao. Wana wa Sauli walikuwa Yonatani na Iswi na Malkisua; wanawe wawili wa kike wa kwanza jina lake ni Merabu, naye mdogo ni Mikali. Naye mkewe Sauli jina lake ni Ahinoamu, binti Ahimasi, nalo jina la mkuu wa vikosi vyake ni Abineri, mwana wa Neri aliyekuwa baba mdogo wa Sauli, kwani Kisi, babake Sauli, na Neri, babake Abineri, walikuwa wana wa Abieli. Vita vya kupigana na Wafilisti vikawa vikali siku zote za Sauli. Kwa hiyo kila mtu, Sauli aliyemwona kuwa fundi wa vita, na kila mtu mwenye nguvu akamchukua kuandamana naye. Samweli akamwambia Sauli: Bwana alinituma, nikupake mafuta, uwe mfalme wao walio ukoo wake wa Waisiraeli. Sasa sikia maneno, Bwana aliyoyasema: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Nitayalipiza, Waamaleki waliyowafanyizia Waisiraeli na kuwazibia njia, walipotoka Misri. Sasa nenda, uwapige Waamaleki! Lakini vyote pia, walivyo navyo, sharti viwe mwiko kwenu wa kuwapo, msivionee uchungu, ila sharti mwaue waume hata wake, watoto hata wachanga, ng'ombe hata kondoo, ngamia hata punda! Sauli akawapasha watu habari hii, akawakagua huko Telaimu, wakawa 200000 wanaokwenda kwa miguu, nao Wayuda 10000. Sauli alipofika penye mji wa Waamaleki, akawavizia mtoni. Nao Wakeni Sauli akawaambia: Haya! Ondokeni, mshuke na kujitenga na Waamaleki, nisije kuwamaliza pamoja nao! Kwani ninyi mliwaendea wana wote wa Waisiraeli kwa upole, walipotoka Misri. Ndipo, Wakeni walipoondoka katikati ya Waamaleki. Kisha Sauli akawapiga Waamaleki toka Hawila, hata mtu afike Suri ulioelekea Misri. Akamteka Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, lakini watu wote akawaua kwa ukali wa panga kwa kuwatia mwiko wa kuwapo. Lakini Sauli pamoja na watu wake wakamhurumia Agagi na mbuzi na kondoo na ng'ombe waliokuwa wazuri kwa kunona na wana kondoo na nyama wengine wa kufuga waliokuwa wazuri, hawakutaka kuwatia mwiko wa kuwapo, wawaue; lakini nyama wote waliokuwa wabayabaya kwa kuugua, ndio, waliowatia mwiko wa kuwapo, wakawaua. Ndipo, neno la Bwana lilipomjia Samweli kwamba: Ninaona majonzi, kwa kuwa nilimweka Sauli kuwa mfalme, kwani ameacha kunifuata, wala hayatimizi maneno yangu. Kwa hiyo moyo wake Samweli ukachafuka, akamlilia Bwana usiku wote. Asubuhi na mapema Samweli akaondoka aje kuonana na Sauli. Samweli akapashwa habari kwamba: Sauli amefika Karmeli, akajisimamishia ukumbusho, kisha akageuka kwenda zake, ashukie Gilgali. Samweli alipofika kwake Sauli, Sauli akamwambia: Ubarikiwe na Bwana! Neno la Bwana nimelitimiza. Samweli akajibu: Je? Hiki kilio cha mbuzi na cha kondoo masikioni mwangu kinatoka wapi? Nacho kilio cha ng'ombe, ninachokisikia, kinatoka wapi? Sauli akasema: Wamewateka kwao Waamaleki; mbuzi na kondoo na ng'ombe walio wazuri watu wamewalimbika kuwa ng'ombe za kumtambikia Bwana Mungu wako; wengine wote tumewatia mwiko wa kuwapo, tukawaua. Ndipo, Samweli alipomwambia Sauli: Acha, nikutolee, Bwana aliyoniambia usiku huu! Akamwambia: Sema! Samweli akasema: Ulipokuwa mdogo machoni pako, ulipata kuwa kichwa chao mashina ya Waisiraeli, Bwana akakupaka mafuta, uwe mfalme wa kuwatawala Waisiraeli, au sivyo? Bwana akakutuma kushika njia aliposema: Nenda, uwatie mwiko wa kuwapo, uwaue hao Waamaleki walio wakosaji! Upigane nao, mpaka uwamalize kabisa! Mbona hukukiitikia kinywa cha Bwana? Mbona umeyageukia hayo mateka, ukayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana? Sauli akamwambia Samweli: Kweli, nimekiitikia kinywa cha Bwana nikaishika njia, Bwana aliyonituma, nikamteka Agagi, mfalme wa Waamaleki, nao Waamaleki nikawatia mwiko wa kuwapo, wauawe; ni watu tu waliovunja mwiko kwa kuchukua katika hayo mateka mbuzi na kondoo na ng'ombe waliokuwa wazuri mno, wawe ng'ombe za kumtambikia Bwana Mungu wako huku Gilgali. Samweli akamwambia: Je? Bwana anapendezwa na vipaji vya tambiko, ijapo ziwe ng'ombe za kuteketezwa nzima, kama anavyopendezwa ukikiitikia kinywa chake Bwana? Tazama, kutii ni kwema kuliko vipaji vya tambiko, nako kusikiliza ni kwema kuliko mafuta ya kondoo; kwani upingani ni ukosaji sawasawa kama uchawi, nao ubishi ni upotovu kama kutambikia mizimu. Kwa kuwa umelitangua neno lake Bwana, naye amekutangua, usiwe mfalme tena. Ndipo, Sauli alipomwambia Samweli: Nimekosa nilipokipita kinywa chake Bwana, nisiyafanye, uliyoniambia; kwani niliwaogopa watu, nikawaitikia sauti zao. Sasa liondoe hili kosa langu! Rudi pamoja na mimi, nije kumwangukia Bwana! Samweli akamwambia Sauli: Sitarudi pamoja na wewe, kwani umelitangua neno lake Bwana, naye Bwana amekutangua, usiwe mfalme tena wa kuwatawala Waisiraeli. Samweli alipogeuka, ajiendee, Sauli akamkamata pindo la kanzu yake, ikararuka. Samweli akamwambia: Bwana amekunyang'anya leo ufalme wa Waisiraeli, akampa mwenzako aliye mwema kuliko wewe. Naye yeye aliye utukufu wa Waisiraeli hasemi uwongo, wala hageuzi moyo, kwani si mtu, ageuze moyo. Sauli akasema: Nimekosa kweli, lakini sasa unipe macheo kwenye hawa wazee wao walio ukoo wangu nako kwao Waisiraeli ukirudi pamoja nami, nije kumwangukia Bwana Mungu wako! Ndipo, Samweli aliporudi na kumfuata Sauli, naye Sauli akaja kumwangukia Bwana. Samweli akasema: Nileteeni Agagi, mfalme wa Waamaleki! Agagi akafika kwake na kuchangamka, akasema: Kweli uchungu wa kufa umenitoka! Lakini Samweli akamwambia: Kama upanga wako ulivyowanyang'anya wanawake wana wao, ndivyo, mama yako anavyongang'anywa leo mwanawe, aondoke kwa wamama wenzake. Kisha Samweli akamkatakata Agagi hapo Gilgali machoni pa Bwana. Kisha Samweli akaenda Rama, naye Sauli akapanda nyumbani kwake huko Gibea wa Sauli. Samweli hakumwona Sauli tena mpaka siku ya kufa kwake; kwani Samweli alisikitika kwa ajili ya Sauli, kwa sababu Bwana ameona majonzi, kwa kuwa alimweka Sauli kuwa mfalme wa kuwatawala Waisiraeli. Bwana akamwambia Samweli: Utamsikitikia Sauli mpaka lini? Nami ndiye niliyemtangua, asiwe mfalme wa kuwatawala Waisiraeli. Jaza pembe yako mafuta, nikutume kwa Isai wa Beti-Lehemu! Kwani nimejionea mfalme katika wanawe. Samweli akasema: Nitakwendaje? Sauli akivisikia ataniua. Bwana akasema: Chukua mori ya ng'ombe mkononi mwako, useme: Nimekuja kumtambikia Bwana! Mwalike Isai, naye aje kwenye tambiko hilo! Nami nitakujulisha utakayoyafanya, unipakie mafuta yeye, nitakayekuonyesha. Samweli akayafanya, Bwana aliyomwambia. Alipofika Beti-Lehemu, wazee wa mji wakamjia njiani na kutetemeka, wakamwamkia kwamba: Kuja kwako ni kwema? Akawaitikia: Ni kwema, nimekuja kumtambikia Bwana: jieueni, nanyi mje pamoja nami kutambika! Isai na wanawe akawaeua mwenyewe, alipowaalika nao kuja kutambika. Ikawa, walipokuja, alipomwona Eliabu akasema moyoni: Labda ni yeye atakayepakwa mafuta mbele yake Bwana. Lakini Bwana akamwambia Samweli: Usiitazame sura yake wala ukubwa wa umbo lake! Kwani nimemkataa; maana Bwana havitazami vile, mtu anavyovitazama, kwani mtu huvitazama vilivyopo machoni, lakini Bwana huvitazama vilivyomo moyoni. Kisha Isai akamwita Abinadabu, akampitisha machoni pa Samweli, naye akasema: Huyu naye siye, Bwana aliyemchagua. Kisha Isai akampitisha Sama, lakini akasema: Huyu naye siye, Bwana aliyemchagua. Vivyo hivyo Isai akawapitisha wanawe wote saba machoni pa Samweli, lakini Samweli akamwambia Isai: Hawa sio, Bwana aliowachagua. Kisha Samweli akamwuliza Isai: Wanao wote ni hao tu? Akasema: Amesalia yule mdogo, naye anachunga kondoo. Samweli akamwambia Isai: Tuma, wamlete! Kwani hatutakaa mezani, mpaka atakapofika hapa. Basi, akatuma, wakamleta, naye alikuwa mwekundu mwenye macho mazuri na umbo jema. Ndipo, Bwana alipomwambia: Haya! Umpake mafuta! Kwani huyu ndiye. Samweli akaichukua pembe yake ya mafuta, akampaka mafuta katikati ya kaka zake. Ndipo, Roho ya Bwana ilipomjia Dawidi kuanzia siku hiyo, ikamkalia siku zote. Kisha Samweli akaondoka kwenda Rama. Royo yake Bwana ikaondoka mwake Sauli, nayo roho mbaya iliyotoka kwa Bwana ikamhangaisha. Ndipo, watumishi wa Sauli walipomwambia: Tazama, roho mbaya ya Mungu inakuhangaisha! Wewe bwana wetu na uwaagize watumishi wako wanaokutumikia, watafute mtu aliye fundi wa kupiga zeze. Napo, itakapokujia ile roho mbaya ya Mungu, basi, akikupigia zeze kwa mkono wake, utaona vema. Sauli akawaambia watumishi wake: Nitafutieni mtu anayejua vema kupiga zeze, kamleteni kwangu! Mmoja wao wale vijana akajibu akisema: Nimemwona mwana wa Isai wa Beti-Lehemu, ya kuwa anajua kupiga zeze, tena ni fundi wa vita menye nguvu za kupigana vitani na za kusemea watu, ni mtu mzuri wa kupendeza, naye Bwana yuko pamoja naye. Ndipo, Sauli alipotuma wajumbe kwa Isai na kumwambia: Mtume mwanao Dawidi achungaye kondoo, aje kwangu! Isai akatoa punda wa kuchukua mzigo wa chakula na kiriba cha mvinyo, tena akampa mwana mbuzi mmoja, akavituma kwa Sauli mkononi mwa mwanawe Dawidi. Ndivyo, Dawidi alivyokwenda kwake Sauli, akamfanyizia kazi. Sauli akampenda sana, akawa mchukua mata yake. Sauli akatuma kwa Isai kwamba: Dawidi na akae kwangu, kwani macho yangu yanamwona kuwa mpole. Ikawa kila mara, ile roho ya Mungu ilipomjia Sauli, Dawidi akalichukua zeze lake, akalipiga kwa mkono wake; ndipo, Sauli alipotulia na kuona vema, ile roho mbaya ikaondoka kwake. Wafilisti wakavikusanya vikosi vyao kwenda vitani, wakakusanyika Soko katika nchi ya Yuda, wakapiga makambi Efesi-Damimu katikati ya Soko na Azeka. Sauli naye na watu wa Waisiraeli wakakusanyika, wakapiga makambi kwenye Bonde la Mkwaju, wakajitengeneza kuja kupigana na Wafilisti. Wafilisti wakawa wamesimama mlimani ng'ambo ya huko, nao Waisiraeli wakawa wamesimama ng'ambo ya huku, bonde likiwa katikati yao. Katika makambi ya Wafilisti kukatokea jitu, jina lake Goliati wa Gati, urefu wake ulikuwa mikono sita na nusu. Alikuwa amevaa kofia ya shaba kichwani, tena kifuani fulana ya chuma, nao uzito wa hiyo fulana ulikuwa sekeli 5000, ndio frasila 5 za shaba. Miguuni alikuwa amevaa shaba vilevile penye miundi, namo mabegani kikingio cha shaba. Uti wa mkuki wake ulikuwa nguzo kama mti wa mfuma nguo, nayo ncha ya chuma ya mkuki wake ilikuwa sekeli 600, ndio nusu kubwa ya frasila ya chuma; naye mchukua ngao humtangulia. Akaja kusimama mbele akipaza sauti sana na kuwaita Waisiraeli waliojipanga, akawaambia: Mbona mmetoka, mkajipanga kupiga vita? Mimi si Mfilisti? Nanyi sio watu wa Sauli? Chagueni mtu wa kwenu, ashuke kuja kwangu! Akiweza kupigana na mimi na kunishinda, basi, tutakuwa watumwa wenu; lakini mimi nikimweza na kumshinda, ninyi mtakuwa watumwa wetu, mtutumikie. Kisha huyo Mfilisti akasema: Siku hii ya leo nimewabeza Waisiraeli waliojipanga, nikiwaambia: Nipeni mtu, tupigane naye! Sauli na Waisiraeli wote walipoyasikia hayo maneno ya huyo Mfilisti wakaingiwa na vituko, wakaogopa sana. Dawidi alikuwa mwana wa yule mtu wa Efurata, ndio Beti-Lehemu wa Yuda, jina lake Isai, aliyekuwa mwenye wana wanane; siku zile za Sauli mwenyewe alikuwa mzee mwenye miaka kuliko wengine. Lakini wana watatu wakubwa wa Isai walikuwa wamemfuata Sauli kwenda vitani, nayo majina yao hawa wanawe watatu waliokwenda vitani ni haya: wa kwanza ni Eliabu, wa pili Abinadabu, wa tatu Sama. Naye Dawidi alikuwa mdogo; kwa kuwa wale wakubwa watatu walikuwa wamemfuata Sauli, Dawidi akatoka mara kwa mara kwake Sauli kwenda kuchunga kondoo wa baba yake huko Beti-Lehemu, kisha akarudi. Lakini yule Mfilisti akatoka asubuhi na jioni siku 40 akija kujisimamisha papo hapo. Kisha Isai akamwambia mwanawe Dawidi: Wapelekee kaka zako mzigo huu wa bisi na hii mikate kumi. Upige mbio, uifikishe upesi kambini kwa kaka zako! Navyo hivi vikate kumi vya maziwa yaliyoganda umpelekee mkuu wa elfu, upate kuwatazama kaka zako, kama hawajambo, nao na wakupe kitu cha kwao, ukilete! Kwani Sauli nao hao na Waisiraeli wote walikuwako kule kwenye Bonde la Mkwaju wakipigana na Wafilisti. Kesho yake Dawidi akaamka na mapema akimwachia mwangaliaji mwingine kondoo na mbuzi, akavichukua alivyopewa, akaenda zake, kama Isai alivyomwagiza; akafika penye magari, vikosi vilipotoka kujipanga na kupiga yowe za vita. Nao Waisiraeli wakajipanga ng'ambo ya huku, nao Wafilisti ng'ambo ya huko, wakaelekeana. Dawidi akautua ule mzigo, akauacha mkononi mwake mlinda mizigo, akakimbilia hapo, walipojipanga, alipofika akaamkiana na kaka zake. Akingali katika kusema nao, mara hapo, Wafilisti walipojipanga, lile jitu likatokea, jina lake Goliati, Mfilisti wa Gati, akayasema maneno yaleyale; Dawidi naye akayasikia. Watu wote wa Waisiraeli walipomwona mtu huyo wakamkimbia wote, kwani wakaogopa sana. Kukawa na mtu wa Kiisiraeli akasema: Mmemwona huyo mtu aliyepanda? Hupanda tu kuwatweza Waisiraeli. Mtu atakayempiga mfalme atampa mali nyingi, hata mwanawe wa kike atampa, awe mkewe, nao mlango wa baba yake utafunguliwa, usitoe kodi kwao Waisiraeli. Dawidi akawauliza wale watu waliosimama pamoja naye akisema: Mtu akimpiga huyo Mfilisti na kuiondoa soni kwao Waisiraeli atafanyiziwa nini? Kwani huyo Mfilisti asiyetahiriwa ni mtu gani akiwatweza wapiga vita wa Mungu aliye Mwenye uzima? Watu wale wakamwambia neno lilelile la kwamba: Hivi ndivyo, atakavyofanyiziwa mtu atakayempiga. Kaka yake Eliabu aliposikia, alivyosemezana na wale watu, makali yake Eliabu yakawaka moto kwa kumkasirikia Dawidi, akamwuliza: Umeshukia nini? Tena hivyo vikondoo vyetu umemwachia nani huko nyikani? Mimi ninayajua majivuno yako na ubaya wa moyo wako, kwani umeshuka tu kutazama vita. Dawidi akamwuliza: Nimekosa nini sasa? Hilo si neno la kuuliza tu? Kisha akaondoka hapo pake, akaja pengine kuulizana na watu neno lilo hilo, nao wakamjibu maneno yayo hayo ya kwanza. Watu walipoyasikia, Dawidi aliyoyasema, wakaja kwa Sauli kumsimulia habari hizo, kisha wakamchukua. Dawidi akamwambia Sauli: Mtu asipotelewe na moyo kwa ajili yake yeye! Mtoto wako atakwenda kupigana na huyo Mfilisti. Sauli akamwambia Dawidi: Hutaweza kumwendea huyo Mfilisti, upigane naye, kwani u kijana, naye yeye ni mpiga vita tangu utoto wake. Dawidi akamwambia Sauli: Mtoto wako alipokuwa anachunga kondoo wa baba yake, basi, simba au chui walipokuja kukamata kondoo kundini, nikatoka kuwafuata, nikawapiga, nikawaopoa vinywani mwao; kama aliniinukia, nikamkamata ndevu zake, nikampiga, hata nikamwua. Kama mtoto wako alivyowapiga simba na chui, vivyo hivyo hata huyo Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwani amewatweza wapiga vita wa Mungu aliye Mwenye uzima. Kisha Dawidi akasema: Bwana aliyeniponya mikononi mwa simba namo mikononi mwa chui ndiye atakayeniponya namo mkononi mwa huyo Mfilisti. Ndipo, Sauli alipomwambia Dawidi: Basi, nenda! Bwana awe nawe! Sauli akamvika Dawidi mavazi yake ya vitani, kichwani pake akamtia kofia ya shaba, akamvika hata fulana ya chuma. Dawidi akajifunga nao upanga wake juu ya hayo mavazi ya vitani. Lakini alipotaka kwenda, kwani alikuwa hajavijaribu, Dawidi akamwambia Sauli: Siwezi kwenda nayo haya, kwani sikuyajaribu bado; kisha Dawidi akayavua, akayaweka, akaichukua fimbo yake mkononi mwake, akajichagulia mtoni vijiwe vitano vilivyoviringana vizuri, akavitia katika mkoba, aliokuwa nao, maana ni mfuko wake, akashika nalo kombeo, kisha akamwendea yule Mfilisti. Yule Mfilisti naye akaja kumfikia Dawidi karibu, naye mchukua ngao akamtangulia. Yule Mfilisti alipochungulia, amwone Dawidi, akambeza, kwa kuwa ni kijana bado, tena ni mwekundu na mwenye umbo zuri. Ndipo, yule Mfilisti alipomwambia Dawidi: Mimi ni mbwa, ukinijia na fimbo? Kisha Mfilisti akamwapiza Dawidi na kuitaja miungu yake. Mfilisti akamwambia Dawidi: Njoo kwangu! Nyama za mwili wako nitawapa ndege wa angani na nyama wa porini! Lakini Dawidi akamwambia Mfilisti: Wewe unanijia na kushika upanga na mkuki na ngao, lakini mimi ninakujia katika Jina la Bwana Mwenye vikosi, aliye Mungu wao wapiga vita vya Waisiraeli, uliyemtukana! Siku hii ya leo Bwana amekutia mkononi mwangu, nikupige, nikukate kichwa mwilini pako, nayo mizoga ya vikosi vya Wafilisti siku hii ya leo nitawapa ndege wa angani na nyama wa porini, watu wote wa nchini wapate kujua, ya kuwa aliye Mungu yuko kwao Waisiraeli. Nao wote wa mkutano huu watajua, ya kuwa Bwana haokoi kwa nguvu za upanga wala za mkuki, kwani vita hivi ni vyake Bwana, naye amewatia mikononi mwetu. Ikawa, yule Mfilisti alipoinuka, aje kumfikia Dawidi karibu, Dawidi naye akapiga mbio, afike upesi hapo, walipojipanga, akutane na yule Mfilisti. Dawidi akautia mkono wake upesi mkobani, akatoa humo kijiwe, akakitupa kwa kombeo, akampiga yule Mfilisti pajini, nacho kijiwe kikaingia pajini ndani; ndipo, alipoanguka kifudifudi hapo chini. Hivyo ndivyo, Dawidi alivyomshinda yule Mfilisti kwa kombeo na kwa kijiwe, akampiga yule Mfilisti na kumwua pasipo kushika upanga mkononi mwake yeye Dawidi. Kisha Dawidi akapiga mbio, akasimama pake yule Mfilisti, akauchukua upanga wake akiuchomoa alani mwake, akamwua kabisa na kukikata kichwa chake; Wafilisti walipoona, ya kuwa fundi wao wa vita amekufa, ndipo, walipokimbia. Lakini watu wa Waisiraeli na Wayuda wakainuka, wakaondoka na kupiga yowe, wakawakimbiza Wafilisti mpaka kufika Gai na malango ya Ekroni, nao Wafilisti walioumizwa wakaanguka njiani kwenda Saraimu, hata Gati na Ekroni. Kisha wana wa Isiraeli wakarudi walipokwisha kuwafukuza sana Wafilisti, wakayateka yaliyokuwapo makambini mwao. Dawidi akakichukua kichwa chake yule Mfilisti, akakipeleka Yerusalemu, lakini mata yake akayaweka hemani mwake. Sauli alipoona, Dawidi alivyotoka, akutane na yule Mfilisti, akamwuliza Abineri, mkuu wa vikosi: Huyu kijana ni mwana wa nani? Abineri akasema: Hivyo roho yako, mfalme, ilivyo nzima, sijui. Mfalme akamwambia: Uliza, kama hili jana ni mwana wa nani? Dawidi aliporudi akiisha kumwua yule Mfilisti, Abineri akamchukua, akampeleka kwa Sauli, akikishika kichwa chake yule Mfilisti mkononi mwake. Sauli akamwuliza: Wewe kijana, u mwana wa nani? Dawidi akasema: Ni mwana wa mtumishi wako Isai wa Beti-Lehemu. Ikawa, alipokwisha kusema na Sauli, roho yake Yonatani ikafungamana na roho yake Dawidi, Yonatani akampenda, kama alivyojipenda. Naye Sauli akamchukua Dawidi siku hiyo, hakumpa ruhusa tena kurudi nyumbani mwa baba yake. Ndipo, Yonatani na Dawidi walipofanya urafiki wa uchale, kwa kuwa alimpenda, kama alivyojipenda. Yonatani akaivua kanzu, aliyokuwa ameivaa, akampa Dawidi pamoja na mavazi yake ya vitani na upanga wake na upindi wake na mkanda wake. Po pote, Sauli alipomtuma, Dawidi akaenda na kuyamaliza kwa werevu yale aliyotumwa; kwa hiyo Sauli akamweka kuwa mkuu wa askari, vikawapendeza watu wote, hata watumishi wa Sauli. Ikawa, Dawidi aliporudi akiisha kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika mji yote ya Waisiraeli kumwendea mfalme Sauli wakiimba na kuchezacheza na kupiga patu na vigelegele na matoazi. Hao wanawake wakaitikiana katika kuimba kwao kwamba: Sauli ameua elfu lake, lakini Dawidi ameua maelfu yake kumi! Makali ya Sauli yakawaka moto sana, wimbo huo ukawa mbaya masikioni mwake, akasema: Dawidi wamempa maelfu kumi, lakini mimi wamenipa elfu tu. Hivyo itakuwa, ufalme nao uwe wake. Siku hiyo ndipo, Sauli alipoanzia kumnunia Dawidi. Kesho yake ile roho mbaya ya Mungu ikampagaa Sauli, akawa nyumbani mwake kama mwenye wazimu akipayukapayuka, lakini Dawidi akampigia zeze kwa mkono wake, kama alivyozoea siku zote, naye Sauli akawa akishika mkuki mkononi mwake. Mara Sauli akautupa mkuki akisema: Na nimchome Dawidi ukutani! Lakini Dawidi akajiepusha mbele yake mara mbili. Sauli akamwogopa Dawidi, kwa kuwa Bwana alikuwa naye, nako kwake Sauli alikuwa ameondoka. Kwa hiyo Sauli akamwondoa nyumbani mwake, akamweka kuwa mkuu wa askari elfu; ndipo, alipotoka, akaja kuwaongoza hao watu. Naye Dawidi akazifuata kwa werevu njia zote, alizozishika, kwani Bwana alikuwa naye. Sauli alipoona, ya kuwa ni mwenye werevu sana, akazidi kumwogopa. Nao Waisiraeli na Wayuda wote wakampenda Dawidi, kwani alikuwa akiwatangulia kwenda na kurudi vitani Sauli akamwambia Dawidi: Tazama, na nikupe mwanangu mkubwa Merabu, awe mkeo. Ila neno moja tu: Sharti uwe fundi wangu wa vita, umpigie Bwana vita. Maana Sauli alisema moyoni: Mkono wangu usimjie, ila mikono ya Wafilisti na imjie. Dawidi akamjibu Sauli: Mimi ni nani? Nayo mambo yangu ya kujitunza ni ya namna gani? Nao ukoo wa baba yangu una ukuu gani kwao Waisiraeli, mimi nipate kuwa mkwe wa mfalme? Lakini siku zilipotimia za kumpa Dawidi Merabu, binti Sauli, akaolewa na Adirieli wa Mehola. Lakini Mikali, binti Sauli, akampenda Dawidi; walipomsimulia Sauli, jambo hili likampendeza machoni pake, maana naye Sauli alikuwa amesema moyoni: Huyu ndiye, nitakayempa, amnase, mikono ya Wafilisti ipate kumjia. Kwa hiyo Sauli akamwambia Dawidi: Leo utakuwa mkwe wangu kwa kumwoa wa pili. Kisha Sauli akawaagiza watumishi wake: Semeni njama na Dawidi kwamba: Tazama! Mfalme amependezwa na wewe, nao watumishi wake wote wanakupenda. Sasa sharti uwe mkwewe mfalme. Watumishi wa Sauli walipoyasema maneno haya masikioni pa Dawidi, Dawidi akawauliza: Ni neno dogo gani kuwa mkwewe mfalme? Nami ni mtu akosaye mali na macheo. Kisha watumishi wa Sauli wakampasha habari za kwamba: Maneno kama hayo ndiyo, Dawidi aliyoyasema. Ndipo, Sauli aliposema: Mwambieni Dawidi haya: mfalme hataki mali nyingine za ukwe, anataka tu magovi mia za Wafilisti, ajilipize kwao hao adui za mfalme. Lakini Sauli alifikiri moyoni njia ya kumtia Dawidi mikononi mwa Wafilisti. Watumishi wa Sauli walipomsimulia Dawidi maneno hayo, jambo hili likampendeza Dawidi kuwa njia ya kuwa mkwewe mfalme. Siku zilipokuwa hazijatimia bado, Dawidi akaondoka, akaenda yeye na watu wake, akaua kwao Wafilisti watu 200; kisha akayapeleka magovi yao, akampa mfalme na kumhesabia yote pia, apate kuwa mkwewe mfalme. Ndipo, Sauli alipompa mwanawe Mikali, awe mkewe. Sauli akayaona, akayajua, ya kuwa Bwana yuko pamoja na Dawidi; naye Mikali, binti Sauli, akampenda. Ndipo, Sauli alipoendelea kumwogopa Dawidi zaidi, kwa hiyo Sauli akawa mchukivu wake Dawidi siku zote. Ikawa kila mara, wakuu wa Wafilisti walipotoka, Dawidi akawaendea kwa werevu zaidi kuliko watumishi wa Sauli, kwa hiyo jina lake likatukuzwa sana. Sauli akala njama na mwanawe Yonatani na watumishi wake wote ya kumwua Dawidi. Lakini Yonatani, mwana wa Sauli, alikuwa amependezwa sana na Dawidi. Kwa hiyo Yonatani akampasha Dawidi habari kwamba: Baba yangu Sauli anatafuta njia ya kukuua; sasa ujiangalie kesho! Kaa mafichoni na kujificha kabisa! Mimi nitatoka, nisimame kando yake baba yangu huko shambani, utakakokuwa, niseme na baba yangu kwa ajili yako, nipate habari za kukupasha wewe. Kisha Yonatani akamsemea mema kwa baba yake Sauli kwamba: Mfalme asije kumkosea mtumishi wake Dawidi! Kwani hakukukosea neno, ila amekufanyizia mema sana. Alipokwenda kumwua yule Mfilisti alijitoa mwenyewe; ndipo, Bwana alipowapatia Waisiraeli wote wokovu mkubwa, nawe ukaviona, ukafurahi. Mbona unataka kujikosesha kwa kumwaga damu ya mtu asiyekosa ukimwua Dawidi bure tu? Sauli akakiitikia kinywa cha Yonatani, yeye Sauli akaapa kwamba: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, hatauawa kabisa! Kisha Yonatani akamwita Dawidi, akamsimulia maneno haya yote; kisha Yonatani akampeleka Dawidi kwa Sauli, akakaa kwake kama siku zote za mbele. Vita vilipoendelea kuwapo, Dawidi akatoka kupigana na Wafilisti, akawapiga pigo kubwa, nao wakamkimbia. Ndipo, ile roho mbaya ya Bwana ilipomjia Sauli, naye alikuwa anakaa nyumbani mwake akishika mkuki wake mkononi, naye Dawidi alikuwa akimpigia zeze kwa mkono wake. Sauli akataka kumchoma Dawidi ukutani kwa mkuki, lakini Dawidi akajiepusha, Sauli asimpate, mkuki ukauchoma ukuta tu. Ndipo, Dawidi alipokimbia kwa hivyo, alivyopona. Usiku huo Sauli akatuma wajumbe kwenda kuivizia nyumba ya Dawidi, wapate kumwua asubuhi. Lakini mkewe Mikali akampasha Dawidi habari kwamba: Usipojiponya usiku huu, utauawa kesho! Kisha Mikali akamshusha Dawidi dirishani, akaenda zake na kukimbia; ndivyo, alivyopona. Kisha Mikali akakichukua kinyago cha nyumbani, akakilaza kitandani, kichwani pake akaweka mto wa manyoya ya mbuzi, akakifunika kwa nguo. Sauli alipotuma wajumbe kumchukua Dawidi, akawaambia: Ni mgonjwa. Sauli akawatuma wale wajumbe tena kumtazama Dawidi akiwaambia: Mleteni kwangu, akilala kitandani, nipate kumwua! Wajumbe walipoingia nyumbani wakakiona kile kinyago, kimelala kitandani, nao mto wa manyoya ya mbuzi uko kichwani pake. Sauli akamwuliza Mikali: Kwa sababu gani umenidanganya hivyo, ukamwacha mchukivu wangu, apone? Mikali akamwambia Sauli: Ameniambia: Niache, nijiendee! Mbona unataka nikuue? Naye Dawidi alipopona kwa kukimbia akaenda Rama kwa Samweli, akamsimulia yote, Sauli aliyomfanyizia, kisha wakaenda yeye na Samweli, wakakaa Nayoti. Sauli akapashwa habari za kwamba: Tazama, Dawidi yuko Nayoti kule Rama! Ndipo, Sauli alipotuma wajumbe kumchukua Dawidi. Hao walipoona kundi la wafumbuaji wakifumbua mambo, naye Samweli akisimama kwao kama kiongozi wao, ndipo, roho ya Mungu ilipowajia wajumbe wa Sauli, nao wakafumbua mambo. Walipompasha Sauli habari hizi, akatuma wajumbe wengine, lakini nao wakaja kufumbua mambo. Ndipo, Sauli alipoendelea kutuma wajumbe mara ya tatu, lakini nao wakaja kufumbua mambo. Kisha naye mwenyewe akaenda Rama; alipofika penye shimo kubwa la maji lililoko Seku akauliza kwamba: Samweli na Dawidi wako wapi? Wakamwambia: Utawaona Nayoti kule Rama. Alipokwenda Nayoti kule Rama, yeye naye roho ya Mungu ikamjia; ndipo, alipokwenda hapo njiani na kufumbua mambo, hata akifika Nayoti kule Rama. Ndipo, yeye naye alipoyavua mavazi yake, naye akafumbua mambo mbele ya Samweli, akalala chini mwenye uchi mchana huo wote na usiku huo wote, kwa hiyo watu husema: Kumbe Sauli naye yumo katika wafumbuaji! Dawidi akakimbia Nayoti kule Rama, akaja kuonana na Yonatani, akamwuliza: Nimefanya nini? Nimekora manza gani kwake baba yako au nimemkosea nini, akitafuta njia ya kuniua? Akamwambia: Sivyo kabisa, hutauawa. Tazama, baba yangu hafanyi jambo, kama ni kubwa au kama ni dogo, asiponitolea masikioni pangu. Basi, jambo hili baba yangu angenifichaje? Hanalo kweli. Dawidi akasema tena na kuapa: Baba yako anajua kabisa, ya kuwa nimepata upendeleo machoni pako, kwa hiyo alisema: Yonatani asilijue, asisikitishwe. Lakini hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena hivyo, roho yako ilivyo nzima, kwangu kutoka maishani kwenda kufani ni hatua moja tu. Yonatani akamwambia Dawidi: Mwenyewe utakayoniambia, nitakufanyizia. Dawidi akamwambia Yonatani: Tazama, kesho ni mwandamo wa mwezi; hapo inanipasa kula mezani pa mfalme, lakini nipe ruhusa, nijifiche shambani hata siku ya tatu jioni. Baba yako akiniuliza, useme: Dawidi ameomba ruhusa kwangu kwenda upesi Beti-Lehemu, kwani siku hizi liko tambiko lao la ukoo wao mzima. Naye akikuambia: Ni vema, basi, mtumishi wako amepata kutengemana; lakini makali yake yakiwaka moto, ndipo, utakapojua, ya kuwa mabaya yamekwisha kujaa moyoni mwake. Umhurumie mtumishi wako na kufanya hivyo! Kwani mtumishi wako umefanya agano naye machoni pa Bwana. Kama ziko manza, nilizozikora, niue wewe! Lakini usinipeleke kwa baba yako! Yonatani akasema: Hili lisikupate! Hapo, nitakapojua, ya kuwa mabaya yamekwisha kujaa moyoni mwa baba yangu, na nije kwako, nikusimulie yote. Dawidi akamwuliza Yonatani: Ni nani atakayenipasha habari, kama baba yako amekujibu neno gumu? Yonatani akamwambia Dawidi: Haya! Tutoke hapa kwenda shambani! Wakatoka wote wawili kwenda shambani. Yonatani akamwambia Dawidi: Bwana Mungu wa Isiraeli ni shahidi! Kesho wakati kama huu au kesho kutwa nikimchunguza baba yangu na kuona, ya kuwa anayo mema ya kumfanyizia Dawidi, basi, nisipotuma mtu kwako, niyafunue masikioni pako, Bwana na aendelee kumfanyizia Yonatani hivi na hivi! Lakini baba yangu akiona kuwa vema kukufanyizia mabaya, nitayafunua nayo masikioni pako, upate kwenda zako na kutengemana; naye Bwana awe na wewe, kama alivyokuwa na baba yangu! Lakini nawe usinifanyie huruma ya Bwana siku hizi tu, nikiwa nipo bado, nisipate kufa, ila nao mlango wangu usiunyime huruma yako kale na kale, hata hapo, Bwana atakapowatowesha wachukivu wa Dawidi, kila mtu mahali pake juu ya nchi hii! Ndivyo, Yonatani alivyoagana na mlango wa Dawidi akisema: Bwana na awalipishe wachukivu wa Dawidi! Yonatani akamwapisha Dawidi tena kwa hivyo, alivyompenda, kwa kuwa alimpenda, kama alivyojipenda mwenyewe. Kisha Yonatani akamwambia: Kesho ni mwandamo wa mwezi; ndipo, utakapoulizwa, kwani kiti chako kitakuwa hakina mtu. Kesho kutwa sharti ushuke kabisa kuja mahali pale, ulipojificha siku ile, tulipoanza shauri, ukae hapo kando ya jiwe la Ezeli. Nami nitapiga mishale mitatu kando yake, kama nitapiga shabaha. Kisha nitatuma mtoto na kumwambia: Nenda, itafute mishale! Hapo, nitakapomwitia huyu mtoto kwamba: Tazama, mishale iko nyuma yako, iokote upande wa huku! utakuja, kwani kutakuwa kumetengemana, hakuna neno baya hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima! Lakini kama nitamwitia yule kijana kwamba: Tazama, mishale iko mbele yako! basi, jiendee! Kwani Bwana amekutuma. Neno hili, tulilolisemezana mimi na wewe, tazama, Bwana ni shahidi wangu na wako kale na kale! Kisha Dawidi akajificha shambani. Siku ya mwandamo wa mwezi ilipotimia, mfalme akajikalisha penye chakula, ale. Naye mfalme akakaa mahali pake pa siku zote, ni hapo ukutani; naye Yonatani akaja kusimama hapo, naye Abineri akakaa kando yake Sauli; lakini kiti chake Dawidi kikawa hakina mtu. Lakini siku hiyo Sauli hakusema neno, kwani alisema moyoni: Labda liko tukio lililompata, asiwe ametakata, kwa kuwa hakueuliwa. Hata kesho yake, ndio siku ya pili ya mwezi, kiti chake kikawa tena hakina mtu. Ndipo, Sauli alipomwuliza mwanawe Yonatani: Mbona mwana wa Isai hakuja jana na leo chakulani? Yonatani akamjibu Sauli: Dawidi ameomba ruhusa kwangu kwenda Beti-Lehemu, akasema: Nipe ruhusa, kwani liko tambiko la ukoo wetu katika mji huo, kaka yangu akaniagiza kwenda. Sasa kama nimeona upendeleo machoni pako, acha, niende upesi kuonana na ndugu zangu! Kwa hiyo hakufika mezani pa mfalme. Ndipo, makali ya Sauli yalipomwakia Yonatani, akamwambia: Wewe mwana wa mama mpotovu mwenye ukatavu wa kutii, sikujui, ya kuwa umemchagua mwana wa Isai? Ndivyo, unavyojitweza mwenyewe, hata mama yako utamtokeza, akiwa mwenye uchi! Kwani siku zote, huyu mwana wa Isai akiwa yu hai hapa nchini, wewe hutashupaa wala ufalme wako. Sasa hivi tuma mtu, amchukue kumleta kwangu! Kwani hana budi kufa. Yonatani akamjibu baba yake Sauli akimwuliza: Auawe kwa sababu gani? Amefanya nini? Ndipo, Sauli alipomtupia Yonatani mkuki wake, amchome; kwa hiyo Yonatani akajua, ya kuwa baba amekwisha kukata shauri la kumwua Dawidi. Yonatani akaondoka hapo mezani kwa makali yaliyowaka moto, hakula chakula cho chote siku hiyo ya pili ya mwandamo wa mwezi, kwani alimsikitikia Dawidi, kwa kuwa baba yake amemtukana. Asubuhi yake Yonatani akatoka kwenda shambani pamoja na mtoto mdogo saa ileile, aliyoagana na Dawidi. Akamwambia mtoto: Upige mbio kuitafuta mishale, nitakayoipiga. Mtoto alipopiga mbio, yeye akapiga mshale na kupita hapo, alipo. Mtoto alipofika hapo, mshale, Yonatani alioutupa, ulipo, Yonatani akamwitia mtoto kwamba: Mshale hauko mbele yako? Kisha Yonatani akamwitia mtoto kwamba: Kaza mwendo upesiupesi, usisimame! Mtoto wa Yonatani alipokwisha kuiokota mishale akaja kwa bwana wake. Lakini mtoto hakujua maana, ni Yonatani na Dawidi tu waliolijua hilo jambo. Kisha Yonatani akampa huyu mtoto aliyekuwa naye mata yake, akamwambia: Nenda, uyapeleke mjini! Mtoto alipokwisha kwenda, Dawidi akatokea upande wa kusini, akauinamisha uso wake chini mara tatu na kumwangukia mara tatu, kisha wakanoneana na kulia machozi pamoja wao wawili, lakini Dawidi akazidi. Kisha Yonatani akamwambia Dawidi: Nenda na kutengemana! Na viwe, tulivyoapiana sisi wawili na kulitaja Jina la Bwana kwamba: Bwana na atushuhudie mimi na wewe, wazao wangu na wazao wako kale na kale! Kisha Dawidi akaondoka kwenda zake, naye Yonatani akaenda mjini. Dawidi akaja Nobe kwa mtambikaji Ahimeleki; Ahimeleki akashikwa na woga, akamwendea Dawidi njiani, akamwuliza: Mbona unakuja peke yako, usiwe na mtu wa kufuatana na wewe? Dawidi akamwambia mtambikaji Ahimeleki: Mfalme ameniagiza neno na kuniambia: Mtu asilijue hili neno, ninalokutuma nililokuagiza! Wako vijana, niliowaagiza, waje mahali fulani. Una chakula gani sasa? Kama ni mikate mitano, nipe, niende nayo, au cho chote kingine kinachoonekana! Mtambikaji akamjibu Dawidi akisema: Sinayo mikate ya kula, ila iko mikate mitakatifu tu; ingewezekana, kama vijana wale wangalijiangalia, wasiguse wanawake. Dawidi akamjibu mtambikaji akimwambia: Tangu jana na juzi tumenyimwa wanawake; napo, nilipotoka, miili ya vijana hao ilikuwa mitakatifu, nayo hii njia yetu ni ya kujiendea tu, pasipo shaka wametakata miili yao hata leo. Ndipo, mtambikaji alipompa ile mikate mitakatifu, kwani haikuwako mikate mingine, isipokuwa ile mikate, aliyowekewa Bwana, nayo huondolewa machoni pa Bwana, wakiweka hapo mikate mingine yenye moto; ni siku ileile, hiyo ya mbele inapochukuliwa. Siku ile kukawako mmoja wao watumishi wa Sauli, naye alikuwa ametengwa, akae machoni pa Bwana, jina lake Doegi wa Edomu aliyekuwa mkuu wa wachungaji wa Sauli. Kisha Dawidi akamwuliza Ahimeleki: Hunao mkuki au upanga? Kwani sikuchukua upanga wangu wala mata yangu mengine, kwani shauri la mfalme lilikuwa la haraka. Mtambikaji akamwambia: Upanga wa yule Mfilisti Goliati, uliyemwua katika Bonde la Mkwaju, uko, umezingwa na nguo, uko nyuma ya kisibau cha mtambikaji; kama unataka kuuchukua, jichukulie! Kwani hakuna mwingine, usipokuwa huo. Dawidi akasema: Hakuna mwingine wa kufanana nao, nipe, niuchukue! Kisha Dawidi akaondoka, akamkimbia Sauli siku hiyo, akaja kwa Akisi, mfalme wa Gati. Watumishi wa Akisi wakamwambia: Kumbe huyu siye Dawidi, mfalme wa nchi ile? Siye yeye, waliyemwimbia na kuitikiana na kumchezea kwamba: Sauli ameua elfu lake, lakini Dawidi ameua maelfu yake kumi? Dawidi alipoyafikisha maneno haya moyoni mwake, akamwogopa sana Akisi, mfalme wa Gati. Kwa hiyo akayageuza mawazo yake mbele yao, akawa kama mwenye wazimu huko kwao, akaipiga milango ya lango la mji kama ngoma, nayo mate yake akayachuruzisha madevuni mwake. Akisi akawaambia watumishi wake: Mnamwona mtu huyu kuwa mwenye kichaa, sababu gani mmemleta kwangu? Je? Mimi nimekosa wenye kichaa, mkimleta huyu, anitolee wazimu wake? Ananijiliaje nyumbani mwangu? Dawidi akatoka huko, akaja kuponea pangoni kwa Adulamu. Kaka zake na mlango wote wa baba yake walipovisikia, wakashuka kwake. Tena wakakusanyika kwake watu wote pia waliosongeka nao wote waliokuwa wenye madeni nao wote waliokuwa na uchungu rohoni mwao, akawa mkuu wao, hivyo akapata watu kama 400 waliokuwa naye. Kisha Dawidi akatoka huko, akaja Misipe wa Moabu, akamwambia mfalme wa Moabu: Acha, baba yangu na mama yangu waje kukaa kwenu, hata nitakapojua, Mungu atakayonifanyizia. Kisha akawapeleka kwa mfalme wa Moabu, wakakaa naye siku zote, Dawidi alipokuwa hapo ngomeni. Kisha mfumbuaji Gadi akamwambia Dawidi: Usikae hapa ngomeni! Ondoka, uende kukaa katika nchi ya Yuda. Ndipo, Dawidi alipokwenda mwituni kwa Hereti. Sauli aliposikia, ya kuwa Dawidi amejulikana, alipo pamoja na watu waliofuatana naye, yeye Sauli alikuwa anakaa Gibea chini ya miombo kilimani, akiushika mkuki wake mkononi, nao watumishi wake wote wakawa wakisimama na kumzunguka. Ndipo, Sauli alipowaambia watumishi wake waliosimama na kumzunguka: Sikilizeni, ninyi Wabenyamini! Mwana wa Isai atawezaje kuwapa ninyi nyote mashamba na mizabibu? Tena atawezaje kuwaweka ninyi nyote kuwa wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia? Kwani ninyi nyote mmenivunjia maagano, kwani hakuna aliyeyafunua masikioni pangu, ya kuwa mwanangu alifanya agano na mwana wa Isai wala hakuna kwenu aliyenionea uchungu akiyafunua masikioni pangu, ya kuwa mwanangu alimchochea mtumishi wangu, aniotee, kama yanavyoelekea leo. Ndipo, Doegi wa Edomu aliyesimama pamoja na watumishi wa Sauli alipojibu akisema: Nimemwona mwana wa Isai, alipoingia Nobe kwa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu. Huyu akamwuliza Bwana kwa ajili yake, akampa pamba za njiani, nao upanga wa yule Mfilisti Goliati akampa. Mfalme akatuma kumwita mtambikaji Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, na mlango wote wa baba yake waliokuwa watambikaji huko Nobe, nao wakaja wote kwa mfalme. Sauli akasema: Sikiliza, mwana wa Ahitubu! Akajibu: Nipo hapa, bwana wangu, Sauli akamwuliza: Mbona mmenivunjia maagano, wewe na mwana wa Isai? Nawe umempa chakula na upanga, ukamwuliza Mungu kwa ajili yake, apate kuniinukia na kuniotea kama yanavyoelekea leo. Ahimeleki akamjibu mfalme akisema: Miongoni mwa watumishi wako wote yuko nani aliye mwelekevu kama Dawidi? Naye ni mkwe wa mfalme, tena huingia katika njama zako, huheshimiwa nyumbani mwako. Je? Siku hiyo ilikuwa ya kwanza ya kumwuliza Mungu kwa ajili yake? Hilo lisinipate! Mfalme asimsingizie mtumishi wake na mlango wote wa baba yangu jambo kama hilo! Kwani mtumishi wako hayajui haya yote, wala makubwa, wala madogo. Lakini mfalme akasema: Utakufa kweli, wewe Ahimeleki na mlango wote wa baba yako. Kisha mfalme akawaagiza wapiga mbio waliosimama hapo na kumzunguka: Wageukieni hawa watambikaji wa Bwana, mwaue! Kwani mikono yao nayo humsaidia Dawidi, tena walijua, ya kuwa anakimbia, lakini hawakuyafunua masikioni pangu. Lakini watumishi wa mfalme wakakataa kuinyosha mikono yao kuwakumba watambikaji wa Bwana. Ndipo, mfalme alipomwambia Doegi. Waangukie wewe, uwakumbe hawa watambikaji! Basi, Doegi wa Edomu akawaangukia, akawakumba hawa watambikaji, akawaua siku hiyo watu 85 waliovaa visibau vya mtambikaji vya ukonge. Kisha akaupiga ule mji wa Nobe kwa ukali wa upanga, waume kwa wake, vijana kwa wachanga, ng'ombe na punda na kondoo, wote pia akawaua kwa ukali wa upanga. Akapona mtoto mmoja tu, mwana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, jina lake Abiatari, naye akamkimbilia Dawidi. Abiatari akamsimulia Dawidi, ya kuwa Sauli amewaua watambikaji wa Bwana. Dawidi akamwambia Abiatari: Siku hiyo, nilipojua, ya kuwa Doegi wa Edomu yuko, nikajua, ya kuwa atamsimulia Sauli hayo yote. Kwa hiyo ni mimi niliyewapatia wote walio wa mlango wa baba yako mambo hayo. Kwa hiyo kaa kwangu, usiogope! Kwani atakayeitaka roho yako sharti kwanza aipate roho yangu, kwangu mimi utakuwa umeangaliwa vema. Watu wakamsimulia Dawidi kwamba: Wafilisti wanapiga vita huko Keila, nao hunyang'anya yaliyopo penye kupuria. Dawidi akamwuliza Bwana kwamba: Niende, niwapige hao Wafilisti? Bwana akamwambia Dawidi. Nenda, uwapige hao Wafilisti, uuokoe mji wa Keila! Lakini watu wa Dawidi wakamwambia: Tazama, huku katika nchi ya Yuda tunakaa na kuogopa; basi, tutakwendaje Keila, Wafilisti walikojipanga? Ndipo, Dawidi alipomwuliza Bwana mara ya pili; naye Bwana akamjibu na kusema: Ondoka, ushukie Keila! Kwani mimi nitawatia Wafilisti mkononi mwako. Kisha Dawidi akaenda Keila na watu wake, akapigana na Wafilisti, akateka mbuzi na kondoo wao, akawapiga pigo kubwa; ndivyo, Dawidi alivyowaokoa wenyeji wa Keila. Ikawa, Abiatari, mwana na Ahimeleki, alipomkimbilia Dawidi kule Keila alishuka na kukishika kisibau cha mtambikaji mkononi. Sauli alipopashwa habari, ya kuwa Dawidi ameingia Keila, Sauli akasema: Mungu amemwumbua na kumtia mkononi mwangu, kwani alipoingia mji wenye milango na makomeo amekwisha kufungiwa humo. Kisha Sauli akawaita watu wote kuja vitani, waushukie Keila kumsonga Dawidi na watu wake kwa kuwazinga. Dawidi alipojua, ya kuwa Sauli amewaza kumfanyizia mabaya, akamwambia mtambikaji Abiatari: Kilete kisibau cha mtambikaji! Kisha Dawidi akaomba: Bwana Mungu wa Isiraeli, msikilize vema mtumishi wako! Kwani Sauli anatafuta njia ya kuingia Keila, auangamize mji huu kwa ajili yangu mimi. Sasa je? Wenyeji wa Keila watanitoa na kunitia mkononi mwake Sauli, atakaposhuka, kama mtumishi wako alivyosikia? Bwana Mungu wa Isiraeli, hili mwambie mtumishi wako! Bwana akasema: Atashuka. Dawidi akauliza tena: Wenyeji wa Keila watanitoa mimi na watu wangu na kututia mkononi mwa Sauli? Bwana akasema: Watawatoa. Ndipo, Dawidi alipoondoka na watu wake waliokuwa kama 600, wakatoka Keila, wakajiendea kwa kujiendea tu. Sauli alipopashwa habari, ya kuwa Dawidi amejiponya na kutoka Keila akaacha kuuendea. Kisha Dawidi akakaa nyikani magengeni, zaidi akakaa milimani katika nyika ya Zifu. Sauli akamtafuta siku zote, lakini Mungu hakumtia mkononi mwake. Dawidi alipoona, ya kuwa Sauli ametoka, apate kuizimisha roho yake, alikuwa mwituni katika nyika ya Zifu. Ndipo, Yonatani, mwana wa Sauli, alipoondoka kwenda kwake Dawidi kule mwituni, akaushupaza mkono wake kwa nguvu za Mungu. Akamwambia: Usiogope! Kwani mkono wa baba yangu Sauli hautakupata, ila wewe utakuwa mfalme wao Waisiraeli, nami nitakuwa wa pili akufuataye; hata baba yangu Sauli anayajua haya. Kisha wote wawili wakafanya agano machoni pa Bwana; Dawidi akakaa kule mwituni, naye Yonatani akaenda nyumbani kwake. Kulikuwako Wazifu waliopanda Gibea kwa Sauli kumwambia: Je? Dawidi hajifichi kwetu magengeni mwituni katika kilima cha Hakila kilichoko kusini kwenye jangwa? Sasa wewe mfalme, shuka tu kwa hivyo, roho yako inavyotamani kabisa kushuka! Nasi tutamtoa, tumtie mkononi mwa mfalme. Sauli akasema: Na mbarikiwe na Bwana, kwa kuwa mmenihurumia! Nendeni kumvumbua tena, mpate kujua na kupaona mahali pake panapo nyayo zake, mmjue naye aliyemwona. Kwani watu huniambia, ya kuwa ni mwerevu sanasana. Tazameni, myajue maficho yote pia, anamojificha! Kisha rudini kwangu kwa hayo, mliyoyavumbua, nipate kwenda nanyi! Kama yuko katika nchi hii, nitamtafuta, nimpate katika maelfu yote ya Yuda. Kisha wakaondoka, wakaenda Zifu mbele ya Sauli; lakini Dawidi na watu wake walikuwa porini katika nyika ya Maoni upande wa kusini kwenye jangwa. Sauli alipokwenda na watu wake kumtafuta, watu wakampasha Dawidi habari; ndipo, aliposhuka mwambani, akakaa katika nyika ya Maoni. Sauli aliposikia, akaja upesi kumfuata kule nyikani kwa Maoni. Sauli akashika njia ya upande wa huku wa mlima ule, naye Dawidi na watu wake wakashika njia ya upande wa huko wa mlima uleule, lakini Dawidi akajihimiza kumkimbia Sauli. Hapo, Sauli na watu wake walipomfikia Dawidi na watu wake na kuwazunguka, wawakamate, ndipo, mjumbe alipofika kwa Sauli kwamba: Uje mbiombio, kwani Wafilisti wanaiteka nchi hii! Ndipo, Sauli alipoacha kumkimbiza Dawidi, akawageukia Wafilisti, kwa hiyo wakapaita mahali pale Mwamba wa Matengano. Kisha Dawidi akaondoka hapo, akakaa magengeni huko Engedi. Ikawa, Sauli aliporudi kwa kuwafuatia Wafilisti, wakampasha habari kwamba: Tazama, Dawidi yuko Engedi nyikani! Ndipo, Sauli alipochukua watu 3000 waliochaguliwa katika Waisiraeli wote, akaenda kumtafuta Dawidi na watu wake kwenye miamba ya minde. Alipofika njiani kwenye mazizi ya kondoo na mbuzi, kulikuwako pango; Sauli akaingia humo kuifunika miguu yake. Namo humo pangoni ndani Dawidi alikuwamo akikaa na watu wake. Watu wa Dawidi wakamwwambia: Basi, leo hivi ni siku hiyo, Bwana aliyokuambia: Utaniona mimi, nikimtia mchukivu wako mkononi mwako, umfanyizie yaliyo mema machoni pako. Dawidi akainuka, akakata pindo la kanzu yake Sauli, asivijue. Lakini baadaye moyo ukamkung'uta Dawidi, kwa kuwa amelikata pindo la kanzu ya Sauli; akawaambia watu wake: Bwana na anizuie kabisa nisimfanyizie bwana wangu, Bwana aliyempaka mafuta, jambo kama hilo la kuuinua mkono wangu, nimguse tu! Kwani Bwana alimpaka mafuta yeye. Kwa maneno haya Dawidi akawazuia watu wake, hakuwapa ruhusa kumwinukia Sauli. Kisha Sauli akaondoka mle pangoni, akaenda zake. Baadaye Dawidi naye akaondoka, akatoka mle pangoni, akapaza zauti nyuma yake Sauli kwamba: Bwana wangu mfalme! Sauli alipotazama nyuma, Dawidi akamwinamia mara mbili na kumwangukia chini. Kisha Dawidi akamwambia Sauli: Mbona unayasikiliza maneno ya watu kwamba: Tazama, Dawidi anakutakia mabaya? Tazama! Leo hivi macho yako yanaweza kuona, ya kuwa Bwana amekutia mkononi mwangu mle pangoni. Lakini watu waliposema, nikuue, jicho langu likakuonea uchungu, nikasema: Sitaukunjua mkono wangu, nimguse tu bwana wangu, kwani Bwana alimpaka mafuta. Baba yangu, tazama, uone nawe! Pindo la kanzu yako limo mkononi mwangu! Kwani nilipolikata hili pindo la kanzu yako, sikukuua. Kwa kuliona ujue, ya kuwa mkononi mwangu hamna kibaya wala kipotovu, wala sijakukosea. Mbona wewe unaniwinda, unipate? Bwana na atuamue, mimi na wewe! Yeye Bwana na anilipizie kwako! Lakini mkono wangu hautakuinukia. Ni hivyo, kama fumbo la kale linavyosema: Kwao waovu hutoka uovu, lakini mkono wangu hautakujia. Mfalme wa Waisiraeli ametoka kumtafuta nani? Wewe unamkimbiza nani? Ni mbwa mfu au kiroboto kimoja tu! Basi, Bwana na atuhukumu na kutuamua mimi na wewe akitutazama! Kisha na anigombee huu ugomvi wangu na kuniponya mkononi mwako! Ikawa, Dawidi alipokwisha kumwambia Sauli maneno haya, Sauli akasema: Kumbe hii si sauti yako, mwanangu Dawidi? Kisha Sauli akapaza sauti na kulia machozi. Akamwambia Dawidi: Wewe u mwenye wongofu kuliko mimi, kwani wewe umenifanyizia mema mimi niliyekufanyizia mabaya. Wewe umeuonyesha leo huo wema, ulionifanyizia, usiponiua, Bwana aliponitoa na kunitia mkononi mwako. Je? Mtu akimwona mchukivu wake atamwacha, ajiendee, pasipo kumfanyizia kibaya? Bwana na akulipe na kukupatia mema kwa hayo, uliyonifanyizia leo. Sasa tazama! Ninajua, ya kuwa utapata kuwa mfalme, nao ufalme wa Waisiraeli utashupaa kwa nguvu za mkono wako. Sasa uniapie ukimtaja Bwana, ya kuwa hutawaangamiza wao wa uzao wangu watakaokuwa nyuma yangu, wala hutalitowesha jina langu katika mlango wa baba yangu. Dawidi akamwapia Sauli haya, kisha Sauli akaenda nyumbani kwake, naye Dawidi akapanda gengeni pamoja na watu wake. Siku zile Samweli akafa; ndipo, Waisiraeli wote walipokusanyika kumwombolezea na kumzika nyumbani kwake huko Rama. Kisha Dawidi akaondoka, akatelemka kwenda nyikani kwa Parani. Kule Maoni kulikuwa na mtu, nako, alikopatia mali, ni Karmeli; mtu huyo alikuwa mkuu kabisa mwenye kondoo 3000 na mbuzi 1000. Naye siku hizo alikuwa huko Karmeli akiwakata kondoo wake manyoya. Huyo mtu jina lake Nabali, naye mkewe jina lake Abigaili; huyu mkewe alikuwa mwenye akili njema na mwenye umbo zuri, lakini yule mume alikuwa mkorofi mwenye matendo mabaya tu, naye ni wa mlango wa Kalebu. Dawidi aliposikia kule nyikani, ya kuwa Nabali yumo katika kukata manyoya ya kondoo wake, Dawidi akatuma vijana kumi; Dawidi akawaambia hao vijana: Pandeni Karmeli, mwende kwa Nabali kunisalimia kwake! Mmwambieni huyu ndugu yangu: Hujambo wewe? Nao wa mlango wako hawajambo? Nao wote walio wako hawajambo? Sasa nimesikia, ya kuwa wanakukatia manyoya ya kondoo wako; basi, hao wachungaji wako walikuwa kwetu sisi, nasi hatukuwafanyizia kibaya cho chote, wala hakikupotea cho chote kwao siku zote, walipokuwa huku Karmeli. Waulize vijana wako, nao watakuambia, kwa hiyo hawa vijana na waone upendeleo machoni pako! Kwani tumekuja siku iliyo njema; mkono wako utakayoyaona, tupe sisi watumishi wako naye mtumishi wako Dawidi! Vijana wa Dawidi walipofika kwake wakamwambia Nabali hayo maneno yote katika jina la Dawidi, kisha wakanyamaza. Lakini Nabali akawajibu vijana wa Dawidi kwamba: Dawidi ni nani? Mwana wa Isai ni nani? Leo watumwa waliotoroka kwa bwana zao ni wengi. Sasa je? Vilaji vyangu na vinyaji vyangu na vinono vyangu, nilivyowachinjia wanaokata manyoya ya kondoo wangu, nivichukue, niwape watu, nisiowajua, wanakotoka? Ndipo, vijana wa Dawidi walipogeuka kurudi kwao; walipofika wakampasha habari hizo zote. Ndipo, Dawidi alipowaambia watu wake: Jifungeni kila mtu upanga wake! Nao wakajifunga kila mtu upanga wake, hata Dawidi akajifunga upanga wake; wakamfuata Dawidi watu kama 400 kwenda naye, wengine 200 wakasalia kwenye mizigo yao. Kijana mmoja miongoni mwao wale vijana akamsimulia Abigaili, mkewe Nabali, kwamba: Tazama! Dawidi ametuma wajumbe toka nyikani, waje kumsalimia bwana wetu, lakini akawafokea. Nao wale watu wametufanyizia mema sana, hawakutufanyizia kibaya cho chote, wala hakikupotea kwetu cho chote siku zote, tulizotembea nao tulipokuwa porini. Walikuwa kwetu kama boma usiku na mchana siku zote, tulizokuwa kwao tukichunga kondoo. Sasa yajue hayo, uone utakayoyafanya! Kwani yako mabaya yaliyokwisha kutengenezwa ya kumpata bwana wetu na mlango wake wote; lakini yeye ni mtu asiyefaa, hatuwezi kusema naye. Ndipo, Abigaili alipojihimiza, akachukua mikate 200 na mitungi 2 ya mvinyo na kondoo 5 waliokwisha kutengenezwa na pishi 5 za bisi na maandazi 100 ya zabibu na 200 ya kuyu, yote pia akapagaza punda. Kisha akawaambia vijana wake: Nitangulieni! Mimi nitawafuata nyuma. Lakini mumewe Nabali hakumwambia neno. Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake na kutelemka mahali palipofichwa na mlima, naye Dawidi na watu wake walikuwa wakitelemka papo hapo upande wa huko; ndivyo, alivyokutana nao. Dawidi akawa akiwaza moyoni kwamba: Kumbe mali zote za mtu huyu nimezilinda nyikani bure tu, yote pia yaliyokuwa yake hayakupotea hata moja, naye hayo mema akayalipa kwa kunifanyizia mabaya. Mungu na awafanyizie wachukivu wote wa Dawidi hivi na hivi, nikisaza mpaka mapambazuko ya kesho mtu mmoja tu wa kiume kwao wote walio watu wake! Abigaili alipomwona Dawidi akashuka upesi katika punda wake, akajiangusha kifudifudi mbele ya Dawidi kumwangukia hapo chini. Kisha akasema na kumpigia magoti: Unilipishe mimi tu huo uovu, bwana wangu! Acha, kijakazi wako aseme masikioni pako, uyasikilize maneno ya kijakazi wako! Naomba sana, bwana wangu asiyaweke moyoni mwake mambo ya mtu huyu asiyefaa, huyu Nabali, kwani kama jina lake lilivyo, ndivyo, alivyo kweli: jina lake ni Nabali (Mjinga), nao ujinga anao kabisa. Lakini mimi kijakazi wako sikuwaona wale vijana, wewe bwana wangu uliowatuma. Sasa bwana wangu, kwa hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena kwa hivyo, mwenyewe ulivyo mzima, Bwana amekuzuia, usije kumwaga damu, ukijilipiza kwa mkono wako mwenyewe. Sasa wachukivu wako nao wote wanaomtakia bwana wangu mabaya na wawe kama Nabali! Sasa matunzo haya, kijakazi wako anayomletea bwana wangu, na wapewe vijana wanaozifuata nyayo za bwana wangu. Mwondolee kijakazi wako, kama amefanya kipotovu! Kwani Bwana atamtengenezea bwana wangu nyumba yenye nguvu, kwani bwana wangu anampigia Bwana vita, nayo mabaya hayaoneki kwako siku zako zote. Mtu atakapoondokea akukimbize na kutafuta njia ya kukuua, ndipo, roho ya bwana wangu itakapokuwa imefungwa vema kifungoni kwao wanaoishi kwake Bwana Mungu wako. Lakini roho za wachukivu wako na azitupe, kama kombeo linavyotupa vijiwe, vikitiwa hapo kati. Hapo, Bwana atakapomfanyizia bwana wangu hayo mema yote, aliyokuambia, na kukuweka kuwa mkuu wa kuwatawala Waisiraeli, hapo halitakutonesha, halitaukwaza moyo wa bwana wangu hilo la kwamba: ulimwaga damu bure tu, upate kujiponya mwenyewe, wewe bwana wangu. Kwa hiyo mkumbuke kijakazi wako hapo, Bwana atakapomfanyizia mema bwana wangu. Dawidi akamwambia Abigaili: Na atukuzwe Bwana Mungu wa Isiraeli aliyekutuma siku hii ya leo kukutana na mimi! Na yatukuzwe nayo mawazo yako! Na utukuzwe wewe nawe! Kwani umenizuia leo kukora manza za damu, nikitaka kujiponya kwa nguvu za mkono wangu. Kwa hivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli aliyenizuia, nisikufanyizie kibaya, alivyo Mwenye uzima, kama usingalipiga mbio kuja kukutana na mimi, kweli kwao walio wa Nabali asingesazwa mpaka mapambazuko ya kesho mtu wa kiume hata mmoja tu. Kisha Dawidi akapokea mkononi mwake aliyomletea akimwambia: Nenda na kutengemana nyumbani kwako! Tazama, nimekusikia sauti yako, nikaukweza uso wako! Abigaili alipofika kwa Nabali akamkuta, akinywa na wenzake nyumbani mwake, kama mfalme anavyokunywa na wageni wake, nao moyo wake Nabali ukawa ukichangamka kwa kulewa kabisa. Kwa hiyo hakumwambia neno kubwa wala dogo mpaka mapambazuko ya kesho. Ikawa asubuhi, Nabali alipolevuka kwa zile mvinyo, alizozinywa, mkewe akamsimulia mambo hayo; ndipo, moyo wake ulipozimia kifuani mwake, naye akawa kama jiwe. Siku kumi zilipopita, Bwana akampiga Nabali, akafa Dawidi aliposikia, ya kuwa Nabali amekufa, akasema: Na atukuzwe Bwana, kwa kuwa amenigombea huo ugomvi wenye soni, Nabali alionipatia, akamzuia mtumishi wake, asifanye mabaya, nayo mabaya ya Nabali Bwana akayarudisha kumjia kichwani pake. Kisha Dawidi akatuma watu kusema na Abigaili, apate kumchukua, awe mkewe. Watumishi wa Dawidi walipofika kwake Abigaili huko Karmeli wakasema naye kwamba: Dawidi ametutuma kwako, akuchukue, uwe mkewe. Naye akainuka, akawaangukia hapo chini mara mbili, akasema: Tazameni, kijakazi wenu yuko tayari kuwatumikia watumishi wa bwana wangu na kuwaogesha miguu. Kisha Abigaili akaondoka upesi, akapanda punda, vijana wa kike watano wakimfuata nyayo zake, naye akawafuata wajumbe wa Dawidi, akawa mkewe. Naye Ahinoamu wa Izireeli Dawidi akamchukua, wote wawili wakawa wakeze. Naye Sauli akamwoza mwanawe Mikali aliyekuwa mkewe Dawidi kuwa mkewe Palti, mwana na Laisi wa Galimu. Kulikuwako Wazifu waliokuja Gibea kwa Sauli kumwambia: Je? Dawidi hajifichi katika kilima cha Hakila kinachoelekea jangwani? Ndipo, Sauli alipoondoka, akatelemka kwenda nyikani kwa Zifu; naye alikuwa na watu 3000 waliochaguliwa katika Waisiraeli, wamtafute Dawidi katika nyika ya Zifu. Sauli akapiga kambi njiani kwenye kilima cha Hakila kinachoelekea jangwani, naye Dawidi alikuwa akikaa kule nyikani. Dawidi alipoona, ya kuwa Sauli anamfuata huko nyikani, Dawidi akatuma wapelelezi; ndivyo, alivyojua, ya kuwa Sauli amefika kweli. Kisha Dawidi akaondoka, akaja mahali pale, Sauli alipopiga kambi; ndipo, Dawidi alipopaona mahali pale, Sauli alipolala pamoja na mkuu wa vikosi vyake Abineri, mwana wa Neri; maana Sauli alikuwa akilala katika boma la magari, nao watu walikuwa wamelala na kumzunguka. Ndipo, Dawidi alipopiga shauri akimwuliza Mhiti Ahimeleki na Abisai, mwana na Seruya, ndugu yake Yoabu, kwamba: Ni nani atakayeshuka pamoja nami kuingia kambini kwa Sauli? Abisai akaitikia kwamba: Mimi nitashuka pamoja na wewe. Ulipokuwa usiku, Dawidi na Abisai wakaingia kwenye wale watu, wakamkuta Sauli, akilala usingizi katika boma la magari, nao mkuki wake ulikuwa umechomekwa nchini kichwani pake, naye Abineri pamoja na watu wote walikuwa wamelala na kumzunguka. Ndipo, Abisai alipomwambia Dawidi: Leo hivi Mungu amemtoa mchukivu wako na kumtia mkononi mwako; sasa nitamchoma hapa chini kwa mara moja kwa mkuki wake, nisimchome mara ya pili. Lakini Dawidi akamwambia Abisai: Usimfanyizie kibaya! Kwani yuko nani atakayeukunjua mkono wake, amwue aliyepakwa mafuta na Bwana, pasipo kulipizwa? Kisha Dawidi akasema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, isifanyike! Ila Bwana atampiga, au itakuja siku yake, afe, au atakaposhuka kupiga vita ataangamia. Hili Bwana anizuilie, nisiukunjue mkono wangu, nimwue aliyepakwa mafuta na Bwana! Sasa uchukue tu mkuki uliochomekwa kichwani pake na mtungi wa maji! Kisha twende zetu! Ndipo, Dawidi alipouchukua mkuki na mtungi wa maji kichwani pake Sauli, kisha wakaenda zao, Hakuna aliyewaona, wala hakuna aliyevijua, wala hakuna aliyeamka, kwani wote walikuwa wamelala, kwani Bwana aliwatia usingizi mwingi. Dawidi akaenda ng'ambo ya huko, akasimama mbali mlimani juu, pakawa mahali pakubwa katikati yao. Kisha Dawidi akapaza sauti kuwaita wale watu wa Abineri, mwana wa Neri, kwamba: Hujibu Abineri? Abineri akajibu akiuliza: Wewe ndiwe nani ukimwita mfalme? Dawidi akamwuliza Abineri: Wewe si mtu wa kiume? Kwao Waisiraeli yuko nani afananaye na wewe? Mbona humwangalii bwana wako mfalme, mtu mmoja akifika kumfanyizia mabaya bwana wako mfalme? Neno hili, ulilolifanya, halifai; hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, m watu wa kufa ninyi msiomwangalia bwana wenu aliyepakwa mafuta na Bwana! Sasa tazameni! Mkuki wa mfalme na mtungi wa maji uliokuwa kichwani pake uko hapa! Ndipo, Sauli alipoitambua sauti kuwa ya Dawidi, akasema: Kumbe hii si sauti yako, mwanangu Dawidi? Dawidi akasema: Ni sauti yangu, bwana wangu mfalme. Akaendelea akisema: Mbona bwana wangu anamkimbiza mtumishi wake? Nimefanya nini? Au kiko kibaya gani mkononi mwangu? Sasa bwana wangu mfalme na ayasikilize maneno ya mtumishi wake! Kama ni Bwana aliyekuhimiza kunijia, na asikie mnuko wa kipaji cha tambiko! Lakini kama ni watu, na wawe wameapizwa mbele ya Bwana! Kwani wamenifukuza, siku hizi nisiandamane nao walio fungu lake Bwana, wakaniambia: Jiendee kutumikia miungu mingine! Sasa damu yangu isimwagike chini, nikiwa ninamkalia Bwana mbali! Kwani mfalme wa Waisiraeli ametoka kutafuta kiroboto kimoja, kama watu wanavyowinda kwale milimani. Ndipo, Sauli aliposema: Nimekosa! Rudi, mwanangu Dawidi! Sitakufanyizia mabaya tena, kwa kuwa roho yangu imekuwa machoni pako yenye kima kikuu siku hii ya leo. Nimefanya ujinga kweli kwa kupotelewa kabisa. Dawidi akajibu akisema: Huu ni mkuki wa mfalme! Na aje kijana mmoja ng'ambo ya huku, auchukue! Naye Bwana atamlipa kila mtu yaupasayo wongofu wake na welekevu wake, maana Bwana amekutia leo mkononi mwangu, lakini nikakataa kuukunjua mkono wangu, nimwue aliyepakwa mafuta na Bwana. Utaona! Kama roho yako ilivyokuwa kuu machoni pangu, ndivyo, roho yangu nayo itakavyokuwa kuu machoni pa Bwana, aniponye katika masongano yote. Ndipo, Sauli alipomwambia Dawidi: Na ubarikiwe, mwanangu Dawidi! Utakayoyafanya utayatimiza, maana utakuwa mwenye uwezo wa kweli. Kisha Dawidi akashika njia kwenda zake, naye Sauli akarudi kwao. Dawidi akasema moyoni mwake kwamba: Siku moja nitaangamizwa kwa mkono wa Sauli; sitaona mema, nisipojiponya kabisa na kuikimbilia nchi ya Wafilisti, Sauli akate tamaa za kunitafuta tena katika mipaka yote ya Waisiraeli; ndivyo, nitakavyoponyoka mkononi mwake. Kwa hiyo Dawidi akaondoka, akapita mpaka yeye na watu 600 waliokuwa naye, wakaenda kwa Akisi, mwana wa Maoki, mfalme wa Gati. Dawidi akakaa kwa Akisi huko Gati yeye na watu wake, kila mtu na mlango wake. Yeye Dawidi alikuwa na wakeze wawili, Ahinoamu wa Izireeli na Abigaili, mkewe Nabali wa Karmeli. Sauli alipopashwa habari, ya kuwa Dawidi amekimbilia Gati, hakuendelea tena kumtafuta. Kisha Dawidi akamwambia Akisi: Kama nimeona upendeleo machoni pako, na wanipe pa kukaa katika mji mmoja wa porini, nikae huko! Inakuwaje, mtumishi wako akikaa kwako katika mji wa kifalme? Ndipo, Akisi alipompa Siklagi siku hiyo; ndivyo, Siklagi ulivyopata kuwa wao wafalme wa Wayuda mpaka siku hii ya leo. Hesabu ya siku, Dawidi alizokaa katika nchi ya Wafilisti, ikawa mwaka na miezi minne. Ndipo, Dawidi na watu wake walipopanda, wakawashambulia Wagesuri na Wagirzi na Waamaleki, kwani hawa ndio waliokaa katika nchi hiyo tangu zamani zote, kufika Suri hata nchi ya Misri. Dawidi alipoipiga hiyo nchi, hakuacha mume wala mke, asimwue, akachukua mbuzi na kondoo na ng'ombe na punda na ngamia na nguo, kisha akarudi kufika kwa Akisi. Akisi alipomwuliza: Leo mmeshambulia wapi? Dawidi hujibu: Upande wa kusini wa Yuda, au: Upande wa kusini wa Wayerameli, au: Upande wa kusini wa Wakeni. Dawidi asipoacha mume wala mke, asimwue, ni kwa kwamba asiwapeleke Gati, wakayasimulia matendo yetu kwamba: Hivi ndivyo, Dawidi alivyovifanya. Hii desturi yake Dawidi akaifuata siku zile zote, alizokaa katika nchi ya Wafilisti. Akisi akamtegemea Dawidi kwamba: Kwa kuwa amejipatia mnuko mbaya kwao walio ukoo wake wa Waisiraeli, atakuwa mtumishi wangu kale na kale. Siku zile Wafilisti wakavikusanya vikosi vyao kwenda vitani kupigana na Waisiraeli. Ndipo, Akisi alipomwambia Dawidi: Sharti ujue kabisa, ya kuwa huna budi kwenda pamoja nami vitani kupigana na Waisiraeli; wewe na watu wako. Dawidi akamwambia Akisi: Kweli na uyajue, mtumishi wako atakayoyafanya. Naye Akisi akmwambia Dawidi: Kweli nitakuweka kukiangalia kichwa changu siku zote. Hapo Samweli alipokufa, nao Waisiraeli wote walipomwombolezea na kumzika mjini kwake huko Rama, Sauli alikuwa amewaondoa wote waliojua kukweza mizimu pamoja na wachawi katika hiyo nchi. Wafilisti walipokusanyika, kisha walipokuja kupiga makambi yao Sunemu, Sauli naye akawakusanya Waisiraeli, wakapiga makambi Gilboa. Sauli alipoyaona makambi ya Wafilisti akashikwa na woga, moyo wake ukastuka kabisa. Lakini Sauli alipomwuliza Bwana, Bwana hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu wa mtambikaji mkuu, wala kwa wafumbuaji. Kisha Sauli akawaambia watumishi wake: Nitafutieni mwaguaji wa kike, niende kwake kuulizana naye! Watumishi wake wakamwambia: Kule Endori yuko mwanamke anayejua kukweza mizimu. Ndipo, Sauli alipojitendekeza kuwa mwingine kwa kuvaa nguo nyingine, akachukua watu wawili wa kwenda naye; wakafika kwa yule mwanamke usiku, akamwambia: Niagulie kwa kukweza mizimu, ukinipandishia mzimu, nitakayekuambia! Yule mwanamke akamwambia: Tazama! Unayajua wewe, Sauli aliyoyafanya alipowatowesha watiisha mizimu pamoja na wachawi katika nchi hii; mbona unanitegea tanzi, upate kuniua? Sauli akamwapia na kumtaja Bwana kwamba: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, kwa jambo hili hutakora manza kabisa! Ndipo, yule mwanamke alipomwuliza: Nikupandishie nani? Akasema: Unipandishie Samweli! Yule mwanamke alipomwona Samweli akalia kwa sauti kuu, naye mwanamke akamwambia Sauli kwamba: Mbona umenidanganya? Ndiwe Sauli. Mfalme akamwambia: Usiogope! Sema tu: Unaona nini? Ndipo, mwanamke alipomwambia Sauli: Ninaona, wa Kimungu akipanda kutoka ndani ya nchi. Akamwuliza: Sura yake nini? Akasema: Yuko mtu mzee anayepanda, amevaa kanzu ya mtambikaji. Ndipo, Sauli alipotambua, ya kuwa ndiye Samweli, akamwinamia mara mbili na kumwangukia chini. Samweli akamwuliza Sauli: Mbona unanisumbua kwa kunipadisha? Sauli akasema: Nimesongeka sana, kwani Wafilisti wameniletea vita, naye Mungu ameondoka kwangu, hanijibu tena, wala kwa wafumbuaji, wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita, unionyeshe, nitakayoyafanya. Samweli akamwuliza: Mbona unaniuliza, Bwana akiwa ameondoka kwako na kugeuka kuwa mpingani wako? Bwana atakufanyizia, kama alivyosema kinywani mwangu: Bwana atauondoa ufalme mkononi mwako, ampe mwenzio Dawidi, kwa kuwa hukukitii kinywa chake Bwana, usipowafanyizia Waamaleki, makali yake yenye moto yaliyoyataka. Kwa sababu hiyo Bwana atakufanyizia jambo hili siku hii ya leo: Bwana atawatia wao Waisiraeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti; kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Navyo vikosi vya Waisiraeli Bwana atawatia mikononi mwa Wafilisti. Papo hapo Sauli akaanguka chini kifudifudi, akashikwa na woga kabisa kwa ajili ya maneno ya Samweli, hata nguvu haikuwamo mwake, kwani alikuwa hakula chakula mchana kutwa na usiku kucha. Kisha yule mwanamke akamjia Sauli; alipoona, ya kuwa amezimia kwa woga, akamwambia: Tazama! Kijakazi wako amekiitikia kinywa chako, nikaiweka roho yangu mkononi mwako, nikayaitikia maneno yako, uliyoniambia; sasa wewe nawe kiitikie kinywa cha kijakazi wako, nikuandalie chakula kidogo, ule, upate nguvu ukienda zako. Akakataa akisema: Sitakula. Lakini watumishi wake walipomhimiza pamoja na yule mwanamke, akaviitikia vinywa vyao, akainuka hapo chini, akakaa kitandani. Yule mwanamke alikuwa na ndama mnono nyumbani, akamchinja upesi, akachukua nao unga, akaukanda, akaoka vikate visivyochachwa. Kisha akamletea Sauli na watumishi wake, wakala. Walipokwisha kula wakaondoka, wakaenda zao usiku uleule. Wafilisti wakavikusanya vikosi vyao vyote Afeki, nao Waisiraeli wakapiga makambi yao kwenye chemchemi iliyoko Izireeli. Wao wakuu wa Wafilisti wakafika hapo kuyapanga mamia na maelfu yao; naye Dawidi akafika na watu wake kuwapanga nyuma ya Akisi. Lakini wakuu wa Wafilisti wakasema: Hawa Waebureo ni wa nini? Akisi akawaambia wakuu wa Wafilisti: Huyu siye Dawidi, mtumishi wa Sauli, mfalme wa Waisiraeli? Amekuwa kwangu siku hizi nayo miaka hii, nami sikuona kwake cho chote tangu siku ile, aliponiangukia, hata siku hii ya leo. Lakini wakuu wa Wafilisti wakamkasirikia, nao hao wakuu wa Wafilisti wakamwambia: Mrudishe mtu huyu, akae mahali pake, ulipompatia! Asishuke pamoja nasi kupigana, asiwe mpingani wetu kwenye mapigano. Kwani liko jambo gani liwezalo kumpatia upendeleo wa bwana wake, lisipokuwa hilo la kuvitoa vichwa vya watu hawa? Je? Huyu Dawidi siye, waliyemwimbia na kuitikiana katika michezo kwamba: Sauli ameua elfu lake, lakini Dawidi ameua maelfu yake kumi? Ndipo, Akisi alipomwita Dawidi, akamwambia: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, wewe u mtu mnyofu! Kwa hiyo ilifaa machoni pangu, utoke pamoja nami, uingie katika vita hivi pamoja nami, kwani sikuona kwako kibaya cho chote tangu siku hiyo, ulipokuja kwangu, hata siku hii ya leo; lakini machoni pao wakuu wewe hufai. Sasa rudi, ujiendee na kutengemana, usifanye kilicho kibaya machoni pao wakuu wa Wafilisti! Ndipo, Dawidi alipomwambia Akisi: Nimefanya nini? Au umeona nini kwa mtumishi wako tangu siku hiyo, nilipokutokea, hata siku hii ya leo, nisije kupiga vita nao adui wa bwana wangu mfalme? Akisi akamjibu na kumwambia: Ninakujua, ya kuwa wewe u mwema machoni pangu kama malaika wa Mungu; ni wao wakuu wa Wafilisti waliosema: Asipande pamoja nasi kupiga vita! Sasa uamke na mapema! Nao watumishi wa bwana wako waliokuja pamoja nawe nanyi mwamke na mapema, mkipata kuona, mwende zenu! Kwa hiyo yeye Dawidi na watu wake wakaamka na mapema kwenda zao, warudi katika nchi ya Wafilisti, nao Wafilisti wakapanda kwenda Izireeli. Ikawa Dawidi na watu wake waliporudi Siklagi siku ya tatu, Waamaleki walikuwa wameishambulia ile nchi ya kusini, hata Siklagi, wakauteka mji wa Siklagi, wakauteketeza kwa moto. Wakawateka wanawake waliokuwamo, wadogo kwa wakubwa, lakini hawakuua mtu, wakawachukua tu, kisha wakaenda zao. Dawidi na watu wake walipofika mjini, wakauona mji kuwa umeteketezwa kwa moto, nao wake zao na watoto wao wa kiume na wa kike walikuwa wametekwa. Ndipo, Dawidi pamoja na watu waliokuwa naye walipopaza sauti, wakalia, mpaka wasipokuwa na nguvu tena za kulia. Nao wale wanawake wawili wa Dawidi walikuwa wametekwa, Ahinoamu wa Izireeli na Abigaili, mkewe Nabali wa Karmeli. Dawidi akasongeka sana, kwani wale watu walitaka kumpiga mawe, kwa kuwa wote pia walikuwa na uchungu rohoni, kila mmoja kwa ajili ya watoto wake wa kiume na wa kike. Ndipo, Dawidi alipojipatia nguvu kwa Bwana Mungu wake. Kisha akamwambia mtambikaji Abiatari, mwana wa Ahimeleki: Kilete kisibau cha mtambikaji! Abiatari alipomletea Dawidi hicho kisibau cha mtambikaji, Dawidi akamwuliza Bwana kwamba: Nikikimbia na kukifuata hicho kikosi nitakipata? Akamwambia: Piga mbio! Kwani utakipata kweli, uwaponye mateka. Ndipo, Dawidi alipokwenda yeye na wale watu 600 waliokuwa naye, wakafika mtoni kwa Besori; huko ndiko, walikokaa wao walioachwa nyuma. Lakini Dawidi na watu 400 wakaendelea kupiga mbio, waliokaa ni 200 tu, ndio wale waliochoka sana, wasiweze kuvuka mtoni kwa Besori. Kisha wakaona mtu wa Misri kule porini, wakamchukua na kumpeleka kwa Dawidi, wakampa chakula, naye akala, kisha wakampa hata maji ya kunywa. Walipompa nalo andazi la kuyu na maandazi mawili ya zabibu, roho yake ikamrudia, kwani alikuwa hakula chakula wala hakunywa maji siku tatu mchana kutwa na usiku kucha. Ndipo, Dawidi alipomwuliza: Wewe mtu wa nani? Unatoka wapi? Akasema: Mimi ni kijana wa Misri, mtumwa wa mtu wa Amaleki; bwana wangu akaniacha, kwa kuwa naliugua, leo ni siku ya tatu. Sisi twaliishambulia nchi ya kusini kwao Wakreti nako kwao Wayuda, tena nchi ya kusini kwao Wakalebu, nao mji wa Siklagi tukauteketeza kwa moto. Dawidi akamwuliza: Utatuongoza, tukipate hicho kikosi? Akasema: Niapie na kumtaja Mungu, ya kuwa hutaniua, wala hutanitoa na kunitia mkononi mwa bwana wangu! Kisha nitakuongoza, ukipate hicho kikosi. Kisha akawaongoza, wakawakuta; nao walikuwa wametawanyika katika nchi hiyo yote, wakawa wanakula, wanakunywa, maana walikula sikukuu kwa ajili ya hayo mateka yote yaliyokuwa makubwa, waliyoyateka katika nchi ya Wafilisti na katika nchi ya Yuda. Dawidi akawapiga kuanzia mapema hata jioni ya kesho yake, kwao asipone mtu, ila ni vijana 400 tu waliopanda ngamia na kukimbia upesi. Dawidi akawaponya wote, Waamaleki waliowachukua, nao wakeze wawili Dawidi akawaponya. Hakupotea kwao hata mmoja, wadogo kwa wakubwa, watoto wa kiume wala wa kike; nazo nyara zote pia, walizozichukua kupeleka kwao, basi, hizo zote pia Dawidi akazirudisha; Dawidi akachukua mbuzi na kondoo na ng'ombe wote, wakawachunga kwenda mbele ya kundi lile la kwao, wakasema: Hizi ndizo nyara za Dawidi. Dawidi alipofika kwenye wale watu 200 waliokuwa wamechoka sana, wasiweze kumfuata Dawidi, waliowaacha kule mtoni kwa Besori, wakatoka kumwendea Dawidi njiani nao wale watu waliokwenda naye. Dawidi alipowafikia karibu hao watu, akawaamkia na kuwauliza, kama hawajambo. Lakini miongoni mwao waliokwenda na Dawidi watu wote waliokuwa wabaya wasiofaa wakaanza kusema kwamba: Kwa kuwa hawakwenda nasi, wasigawiwe nyara, tulizozipokonya, ila wapewe tu kila mtu mkewe na wanawe, wawapeleke kwenda zao. lakini Dawidi akasema: Msifanye hivyo, ndugu zangu, kuyatumia hivyo, Bwana aliyotupa! Naye ametulinda, akakitia kile kikosi kilichotujia mikononi mwetu. Yuko nani atakayewaitikia katika jambo hili? Ila fungu lake aliyeshuka kupigana sharti liwe sawa na fungu lake yeye aliyekaa na kulinda mizigo, wote pamoja sharti wagawiwe sawasawa! Tangu siku hiyo hata baadaye yakawa vivyo hivyo; watu wakayaweka hayo kuwa maongozi na maamuzi kwao Waisiraeli hata siku hii ya leo. Dawidi alipofika Siklagi akatuma watu kuwapelekea wazee wa Yuda waliokuwa rafiki zake fungu moja la hizo nyara na kuwaambia: Tazameni! Hili ni gawio lenu la nyara zitokazo kwao wachukivu wake Bwana. Waliopewa ndio wa Beteli na wa Ramoti wa kusini na wa Yatiri na wa Aroeri na wa Sifumoti na wa Estemoa na wa Rakali, na wa miji ya Wayerameli na wa miji ya Wakeni na wa Horma na wa Kori-Asani na wa Ataki na wa Heburoni na wa mahali pote, Dawidi na watu wake walipotembeatembea. Wafilisti walipopigana na Waisiraeli, watu wa Waisiraeli wakawakimbia Wafilisti kwa madonda waliyopigwa, wakaanguka wakafa kule mlimani kwa Gilboa. Wafilisti wakawafuata na kuandamana na Sauli na wanawe, Wafilisti wakawaua wana wa Sauli: Yonatani na Abinadabu na Malkisua. Mapigano yakawa makali hapo, Sauli alipokuwa; wapiga mishale walipomwona, akaumizwa sana nao wapiga mishale. Ndipo, Sauli alipomwambia mchukua mata yake: Uchomoe upanga wako, unichome nao, hao wasiotahiriwa wasije kunichoma na kunichezea vibaya! Mchukua mata yake alipokataa kwa kuogopa sana, Sauli akausimika upanga, akauangukia. Mchukua mata yake alipoona, ya kuwa Sauli amekufa, naye akauangukia upanga wake, akafa pamoja naye. Ndivyo, Sauli alivyokufa na wanawe watatu na mchukua mata yake na watu wake wote, wote pia siku hiyohiyo. Watu wa Waisiraeli waliokaa ng'ambo ya huko ya hilo bonde na ng'ambo ya huko ya Yordani walipoona, ya kuwa Sauli na wanawe wamekufa, wakaiacha miji yao, wakakimbia nao; kisha Wafilisti wakaja, wakakaa humo. Ikawa kesho yake, Wafilisti walipokuja kuwapambua waliouawa wakamwona Sauli na wanawe watatu, jinsi walivyokufa mlimani kwa Gilboa. Wakamkata kichwa, wakampambua mata yake, wakatuma wajumbe kwenda po pote katika nchi ya Wafilisti na kuyatangaza penye nyumba ya vinyago vyao, hata kwa watu. Mata yake wakayaweka nyumbani mwa Maastaroti, nao mzoga wake wakautungika bomani kwa mji wa Beti-Sani. Wenyeji wa Yabesi wa Gileadi walipoyasikia, Wafilisti waliyomfanyizia Sauli, Wakaondoka watu wote walioweza kupiga vita, wakaenda usiku wote, wakauchukua mzoga wa Sauli, nayo mizoga ya wanawe pale bomani kwa Beti-Sani, kisha wakarudi na kuipeleka Yabesi, wakaiteketeza huko kwa moto. Kisha wakaichukua mifupa yao, wakaizika chini ya miombo kwao Yabesi, wakafunga mfungo siku saba. Ikawa, Sauli alipokwisha kufa, Dawidi akarudi kwa kuwapiga Waamaleki; kisha Dawidi akakaa Siklagi siku mbili. Ilipokuwa siku ya tatu, mara akaja mtu aliyetoka makambini kwa Sauli, nguo zake zilikuwa zimeraruliwa, napo kichwani pake palikuwa na vumbi; naye alipofika kwake Dawidi akajitupa chini na kumwangukia. Dawidi alipomwuliza: Unatoka wapi? akamwambia: Nimekimbia makambini kwa Waisiraeli. Ndipo, Dawidi alipomwambia: Nisimulie yaliyofanyika huko! Akamwambia, ya kuwa watu walikimbia penye mapigano, kwa maana wengi wa kwao waliangushwa, wakafa, naye Sauli na mwanawe Yonatani wamekufa. Dawidi akamwuliza huyo kijana aliyempasha habari hizi: Umejuaje, ya kuwa Sauli amekufa na mwanawe Yonatani? Yule kijana aliyempasha hizi habari akamwambia: Ikanitukia, nifike mlimani kwa Gilboa, mara nikamwona Sauli, akiuegemea mkuki wake, nayo magari pamoja na wapanda farasi wakamsonga. Alipogeuka nyuma, akaniona, akaniita; nami nikamwitikia kwamba: Nipo hapa! Akaniuliza: Wewe nani? Nikamjibu: Mimi Mwamaleki. Akaniambia: Njoo hapa, nilipo, uniue! Kwani kizunguzungu kimenipata, nayo roho yangu ingali nzima. Ndipo, nilipokuja hapo, alipokuwa, nikamwua, kwani nilijua, ya kuwa hawezi kupona kwa hivyo, alivyoanguka;. kisha nikakichukua kilemba chake kichwani pake na kikuku chake mkononi pake, nimevileta hapa kwa bwana wangu, ni hivi! Ndipo, Dawidi alipoyakamata mavazi yake, akayararua, nao watu wote waliokuwa naye wakafanya hivyo. Wakaomboleza na kulia machozi, wakafunga mfungo mpaka jioni kwa ajili ya Sauli na kwa ajili ya mwanawe Yonatani na kwa ajili ya watu wa Bwana na kwa ajili yao wa mlango wa Isiraeli, kwa kuwa wameangushwa na panga. Kisha Dawidi akamwuliza huyo kijana aliympasha habari hizi: Wewe u mtu wa wapi? Akasema: Mimi ni mwana wa mtu mgeni wa Amaleki. Dawidi akamwambia: Kumbe hukuogopa kuuinua mkono wako, umwangamize aliyepakwa mafuta na Bwana? Ndipo, Dawidi alipomwita mmoja wao vijana, akamwambia: Njoo, umpige! Naye alipompiga, akafa; kisha Dawidi akamwambia: Damu yako na ikujie kichwani pako! Kwani kinywa chako kimekuponza na kusema kwamba: Mimi nimemwua aliyepakwa mafuta na Bwana. Kisha Dawidi akatunga ombolezo hili la kumwombolezea Sauli na mwanawe Yonatani. Akaagiza kuwafundisha wana wa Yuda wimbo huu wa upindi, nao utaukuta, umeandikwa katika kitabu cha Mnyofu: Isiraeli, waliokuwa pambo lake wameuawa vilimani kwako! Imekuwaje, wakiangushwa hao mafundi wa vita? Msiyasimulie Gati, wala msiyatangaze njiani kwa Askaloni, wasipate kufurahi wanawake wa Wafilisti, wasipige vigelegele wao wanawake wa kimizimu! Msione tena umande wala mvua, ninyi milima ya Gilboa, yasiwe tena kwenu mashamba yenye malimbuko! Kwani ndiko, zilikoachwa ngao zao hao mafundi wa vita, ngao yake Sauli naye, kama hakupakwa mafuta. Upindi wake Yonatani ulikuwa hauponyi, ijapo wawe mafundi wa vita wenye unono, uliotaka kuwaua; upanga wake Sauli haukurudi alani, usipokuwa umeua. Sauli na Yonatani walipatana kwa kupendana mioyoni, hawakutengeka walipoishi, wala walipokufa. Walikuwa wepesi kuliko kozi, walikuwa wenye nguvu kuliko simba. Ninyi wanawake wa Kiisiraeli, mwombolezeeni Sauli! Kwani aliwavika mavazi ya kifalme yenye urembo mwingi, kisha hizo nguo zenu akazipamba kwa mapambo ya dhahabu. Imekuwaje, wakiangushwa vitani hao mafundi wa vita? Yonatani akiuawa vilimani kwako? Moyo wangu umesongeka kwa ajili yako, maana wewe ulinipendeza sana, ndugu yangu Yonatani, upendo wako ulinifurahisha kuliko upendo wa wanawake. Imekuwaje, wakiangushwa hao mafundi wa vita? hayo mata makali ya kupigia vita yakiangamia hivyo? Ikawa, Dawidi alipomwuliza Bwana baadaye kwamba: Nipande kukaa katika mji mmoja wa Yuda? Bwana akamwambia: Panda! Dawidi akauliza tena: Nipande kukaa wapi? Akamwambia: Heburoni. Ndipo, Dawidi alipopanda kukaa huko pamoja na wakeze wawili, Ahinoamu wa Izireeli na Abigaili, mkewe Nabali wa Karmeli. Nao wale watu waliokuwa naye Dawidi akawapandisha kila mtu na mlango wake, wakakaa katika miji ya Heburoni. Kisha waume wa Yuda wakaja, wakampaka Dawidi mafuta, awe mfalme wa mlango wa Yuda. Nao wakampasha Dawidi habari, ya kuwa watu wa Yabesi wa Gileadi wamemzika Sauli. Dawidi akatuma wajumbe kwa watu wa Yabesi wa Gileadi, akawaambia: Na mbarikiwe na Bwana ninyi, kwa kuwa bwana wenu Sauli mmemfanyizia tendo lililo jema la kumzika! Sasa Bwwana na awafanyizie nanyi matendo yanayoelekea kuwa mema kweli, mimi nami na niwarudishie wema huo, kwa kuwa mmefanya jambo hilo. Sasa na mwikaze mikono yenu, mpate nguvu, kwani bwana wenu Sauli amekufa, tena mimi nami wao wa mlango wa Yuda wamenipaka mafuta, niwe mfalme wao. Naye Abineri, mwana wa Neri, aliyekuwa mkuu wa vikosi vya Sauli, akamchukua Isiboseti, mwana wa Sauli, akampeleka Mahanaimu, akamfanya kuwa mfalme wa Gileadi na wa Asuri na wa Izireeli na wa Efuraimu na wa Benyamini na wa Waisiraeli wote. Isiboseti, mwana wa Sauli, alikuwa mwenye miaka 40 alipoupata ufalme wa Waisiraeli, akawa mfalme miaka 2; ni wao wa mlango wa Yuda tu waliomfuata Dawidi. Nayo hesabu ya siku, Dawidi alizokuwa mfalme wa mlango wa Yuda huko Heburoni, ikawa miaka 7 na miezi 6. Abineri, mwana wa Neri, akatoka Mahanaimu na watumishi wa Isiboseti, mwana wa Sauli, kwenda Gibeoni. Ndipo, Yoabu, mwana wa Seruya, alipotoka naye na watumishi wake Dawidi, wakakutana penye ziwa la Gibeoni; hao wakakaa ng'ambo ya huku ya hilo ziwa, nao wale wakakaa ng'ambo ya pili ya hilo ziwa. Abineri akamwambia Yoabu: Na waondokee vijana, wacheze mbele yetu! Yoabu akaitikia: Haya! Na waondokee! Basi, wakaondoka, wakaja kusimama huku na huko kwa kuhesabiwa: 12 wa Benyamini na wa Isiboseti, mwana wa Sauli, tena 12 watumishi wa Dawidi. Wakakamatana kila mtu kichwa cha mwenzake, wakachomana panga kila mtu ubavuni mwa mwenzake, kwa hiyo wakaanguka wote pia, wakafa. Wakapaita mahali pale Fungu lenye Mapanga Makali lililoko Gibeoni. Kisha mapigano yakawa makali sanasana siku hiyo, Abineri na watu wa Waisiraeli wakashindwa na watumishi wake Dawidi. Wakawako wana watatu wa Seruya, Yoabu na Abisai na Asaheli; naye Asaheli alikuwa mwepesi kwa kupiga mbio kama paa wanaokaa porini. Naye Asaheli akamkimbiza Abineri na kumfuata, hakujielekeza kwenda kuumeni wala kushotoni, asiache kumfuata Abineri. Abineri akageuka nyuma, akamwuliza: Wewe siwe Asaheli? Akasema: Ndimi! Abineri akamwambia: Geuka kuumeni kwako au kushotoni kwako, ukamate kijana mmoja, uchukue mata yake! Lakini Asaheli akakataa kuondoka kwake na kuacha kumfuata. Abineri akamwambia Asaheli mara ya pili: Ondoka, uache kunifuata! Kwa nini nikupige, uanguke chini? Nitawezaje kutokea usoni pa kaka yako Yoabu? Alipokataa kabisa kumwondokea, Abineri akamchoma tumboni kwa ncha ya chini ya mkuki, mkuki ukatokea mgongoni; ndipo, alipoanguka chini, akafa papo hapo. Ikawa, wote waliofika hapo, Asaheli alipoanguka chini akifa, wakasimama hapo. Kisha Yoabu na Abisai wakamkimbiza Abineri; jua lilipokuchwa walikuwa wamefika kwenye kilima cha Ama kielekeacho Gia penye njia ya kwenda nyikani kwa Gibeoni. Ndipo, wana wa Benyamini walipokusanyika, wamfuate Abineri, wakawa kikosi kimoja, wakasimama juu ya kilima kimoja. Hapo Abineri akamwita Yoabu kwamba: Je? Upanga na ule kale na kale? Hujui, ya kuwa mwisho wake utakuwa uchungu? Utangoja mpaka lini, uwaambie hao watu, warudi na kuacha kuwafuata ndugu zao? Yoabu akasema: Hivyo, Mungu alivyo Mwenye uzima, kama ungalisema hivyo asubuhi, watu wangalikwenda zao na kuacha kukimbizana kila mtu na ndugu yake. Kisha Yoabu akapiga baragumu; ndipo, watu wote waliposimama, hawakuwakimbiza tena Waisiraeli, wala hawakuendelea kupigana nao. Abineri na watu wake wakashika njia ya kupita jangwani usiku kucha, kisha wakavuka Yordani, wakapita Bitironi yote, kisha wakafika Mahanaimu. Yoabu naye akarudi, akaacha kumfuata Abineri, akawakusanya watu wake wote; ndipo, ilipoonekana kwa watumishi wa Dawidi, ya kuwa watu 19 hawako, tena Asaheli. Lakini watumishi wa Dawidi walipiga kwao Wabenyamini na kwa watu wa Abineri watu 360; ndio waliokufa. Wakamchukua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake lililoko Beti-Lehemu; kisha Yoabu na watu wake wakaenda usiku kucha, nao walipofika Heburoni, kukapambazuka. Vita vya kupigana kwao na mlango wa Sauli nao wa mlango wa Dawidi vikawa vya siku nyingi, lakini Dawidi akaendelea kupata nguvu, nao wa mlango wa Sauli wakaendelea kuwa wanyonge. Naye Dawidi akazaa wana huko Heburoni: mwanawe wa kwanza alikuwa Amunoni wa Ahinoamu wa Izireeli. Naye wa pili alikuwa Kilabu wa Abigaili, mkewe Nabali wa Karmeli, naye wa tatu alikuwa Abisalomu, mwana wa Maka, binti Talmai, mfalme wa Gesuri. Naye wa nne alikuwa Adonia, mwana wa Hagiti, naye wa tano alikuwa Sefatia, mwana wa Abitali. Naye wa sita alikuwa Itiramu, mwana wa Egla, mkewe Dawidi. Hawa ndio waliozaliwa kwake Dawidi huko Heburoni. Ikawa hapo, vita vya kupigana kwao wa mlango wa Sauli nao wa mlango wa Dawidi vilipokuwa, ndipo, Abineri alipoendelea kupata nguvu kwao wa mlango wa Sauli. Sauli alikuwa na suria, jina lake Risipa, binti Aya. Naye Isiboseti akamwuliza Abineri: Mbona umeingia kwake suria ya baba yangu? Ndipo, Abineri alipokasirika sana kwa ajili ya hayo maneno ya Isiboseti, akasema: Je? Mimi ni kichwa cha mbwa wa Kiyuda, kwa kuwa nimewafanyizia matendo mema walio wa mlango wa Sauli na ndugu zake na rafiki zake mpaka siku hii ya leo? Wewe nawe sikukutoa mkononi mwake Dawidi? Nawe unanisingiziaje leo kuwa mwenye manza kwa kukosa na yule mwanamke? Basi, Mungu na amfanyizie Abineri hivi na hivi, nisipomfanyizia Dawidi yaleyale, Bwana aliyoapa kumfanyizia! Nitauondoa ufalme kwao wa mlango wa Sauli, nikisimamishe kiti cha kifalme cha Dawidi, awatawale Waisiraeli na Wayuda toka Dani mpaka Beri-Seba. Naye hakuweza tena kumjibu Abineri hata neno moja kwa kumwogopa. Papo hapo Abineri akatuma wajumbe kwake Dawidi kwamba: Nchi ni ya nani? Haya! Fanya agano lako na mimi! Ndipo, mkono wangu utakapokusaidia kuwageuza Waisiraeli wote, wakufuate. Naye akasema: Basi, mimi nitafanya agano na wewe, lakini liko neno moja, ninalolitaka kwako, ni hili: Hutauona uso wangu, usipomleta kwanza Mikali, binti Sauli. Kisha utakuja kuuona uso wangu. Dawidi akatuma wajumbe kwake Isiboseti, mwana wa Sauli, kumwambia: Nipe mke wangu Mikali niliyempata, awe mke wangu kwa kutoa magovi 100 ya Wafilisti. Ndipo, Isiboseti alipotuma kumchukua kwa mumewe Paltieli, mwana wa Laisi. Huyo mumewe akaenda naye akimsindikiza na kulia machozi mpaka Bahurimu; ndipo, Abineri alipomwambia: Nenda, urudi! Naye akarudi. Kisha Abineri akasema na wazee wa Waisiraeli kwamba: Tangu jana na juzi mlikuwa mkimtaka Dawidi, awe mfalme wenu. Sasa yafanyeni! Kwani Bwana amemwambia Dawidi kwamba: Kwa kuutumia mkono wa mtumishi wangu Dawidi nitawaokoa walio ukoo wangu wa Waisiraeli mikononi mwa Wafilisti namo mikononi mwa adui zao wote. Yayo hayo Abineri akayasema hata msikioni pao Wabenyamini. Kisha Abineri akaenda kusema masikioni pa Dawidi huko Heburoni yote yaliyokuwa mema machoni pao Waisiraeli, hata machoni pao wote walio wa mlango wa Benyamini. Abineri alipofika Heburoni kwake Dawidi pamoja na watu 20, Dawidi akamfanyizia karamu Abineri pamoja na wale watu waliokuwa naye. Ndipo, Abineri alipomwambia Dawidi: Naondoka, niende kuwakusanya Waisiraeli wote kwake bwana wangu mfalme, wafanye agano na wewe, uwe mfalme wao na kufanya yote, roho yako itakayoyatamani. Dawidi akampa Abineri ruhusa kwenda zake, naye akaenda na kutengemana. Mara watumishi wa Dawidi wakaja pamoja na Yoabu kutoka vitani, wakaleta vitu vingi, walivyoviteka; lakini Abineri alikuwa hayuko tena Heburoni kwake Dawidi, kwani alimpa ruhusa kwenda zake, naye alikuwa amekwenda na kutengemana. Yoabu na kikosi chote kilichokuwa naye walipofika, watu wakamsimulia Yoabu kwamba: Abineri, mwana wa Neri, amekuja kwa mfalme, naye akampa ruhusa, akaenda zake na kutengemana. Ndipo, Yoabu alipokuja kwa mfalme, akamwambia: Umefanya nini? Tazama, Abineri alipofika kwako, mbona umempa ruhusa, akapata kwenda zake? Humjui Abineri, mwana na Neri ya kuwa amekuja tu kukudanganya, apate kujua kutoka kwako na kuingia kwako na kuyajua yote, wewe unayoyafanya? Yoabu alipotoka kwa Dawidi, akatuma wajumbe, wamfuate Abineri, wamrudishe kwenye kisima cha Sira, lakini Dawidi hakuvijua. Abineri alipofika Heburoni tena, Yoabu akamchukua langoni katikati na kumpeleka kando, apate kusema naye kinjamanjama; huko akamchoma tumboni, afe kwa ajili ya damu ya ndugu yake Asaheli. Baadaye Dawidi alipoyasikia akasema: Mimi na ufalme wangu hatumo kale na kale katika damu ya Abineri, mwana wa Neri, naye Bwana anavijua. Sharti imrudie Yoabu kichwani pake nao wote walio wa mlango wa baba yake. Katika mlango wa Yoabu asikoseke aliye mwenye kisonono au mwenye ukoma au mwenye mikongojo makwapani au mwenye kuuawa na upanga au mkosefu wa chakula! Lakini Yoabu na ndugu yake Abisai walimwua Abineri, kwa kuwa alimwua ndugu yao Asaheli kule Gibeoni katika mapigano. Dawidi akamwambia Yoabu, nao watu wote waliokuwa naye: Yararueni mavazi yenu! Kisha vaeni magunia, mwombolezeeni Abineri mkimtangulia! Naye mfalme Dawidi akalifuata jeneza lake. Walipomzika Abineri kule Heburoni, mfalme akaipaza sauti yake na kulia kule kaburini kwake Abineri, nao watu wote wakalia. Mfalme akamwombolezea Abineri kwamba: Je? Abineri amekufa kama mpumbavu? Mikono yako haikufungwa, wala miguu yako haikutiwa pingu! Kama mtu anavyoangushwa nao wenye maovu, ndivyo, ulivyoangushwa nawe wewe! Ndipo, watu wote walipoendelea kumlilia. Watu wote walipokuja kumpa Dawidi chakula, mchana ungaliko, Dawidi akaapa kwamba: Mungu na anifanyizie hivi na kupita hivi, nikionja mkate au cho chote kingine kabla ya kuchwa kwa jua. Watu wote walipoyaona kuwa kweli, yakawa mema machoni pao, kama mengine yote, mfalme aliyoyafanya, yalivyokuwa mema machoni pa watu. Siku hiyo watu wote na Waisiraeli wote wakajua, ya kama hilo shauri la kumwua Abineri, mwana wa Neri, halikutoka kwake mfalme. Kisha mfalme akawaambia watumishi wake: Hamjui, ya kuwa siku hii ya leo kwao Waisiraeli ameanguka mkuu mwenye ukubwa wa kweli? Mimi leo ni mnyonge bado, ijapo nimepakwa mafuta, niwe mfalme; lakini hawa wana wa Seruya ni wakali kuliko mimi. Bwana na amlipishe aliyeufanya ubaya huo kwa hivyo, ubaya wake ulivyo. Isiboseti, mwana wa Sauli, aliposikia, ya kuwa Abineri amekufa huko Heburoni, mikono yake ikamlegea, nao Waisiraeli wote wakastushwa. Huyo mwana wa Sauli alikuwa na watu wawili waliokuwa wakuu wa vikosi, mmoja jina lake Baana, wa pili jina lake Rekabu, wana wa Rimoni wa Beroti waliokuwa wana wa Benyamini, kwani nchi ya Beroti ilihesabiwa kuwa ya Benyamini. Nao Waberoti walikuwa wamekimbilia Gitaimu; ndiko, wanakokaa ugenini hata leo hivi. Yonatani, mwana wa Sauli, alikuwa na mtoto mume aliyelemaa miguu yote miwili; huyu alikuwa mwenye miaka mitano, ile habari ya kufa kwao Sauli na Yonatani ilipofika kutoka Izireeli; hapo mlezi wake akamchukua, akimbie naye. Ikawa, alipojihimiza kukimbia, yule mtoto akaanguka, akakipata hicho kilema cha miguu, nalo jina lake Mefiboseti. Wale wana wa Rimoni wa Beroti, Rekabu na Baana, wakaenda; napo, jua la mchana lilipokuwa kali, wakaingia nyumbani mwa Isiboseti, naye alikuwa amelala kupumzikia mchana. Nao wakaingia mpaka katikati ya nyumba wakichukua ngano; ndipo, walipomchoma tumboni, kisha Rekabu na ndugu yake Baana wakakimbia. Vilikuwa hivi: walipoingia nyumbani, yeye alikuwa amelala kitandani pake katika chumba cha kulalia; nao walipokwisha kumwua kwa kumchoma, wakamkata kichwa, wakakichukua kichwa chake, wakaenda zao na kushika njia ya jangwani usiku kucha. Hicho kichwa cha Isiboseti wakakipeleka Heburoni kwa Dawidi, wakamwambia mfalme: Hiki ni kichwa cha Isiboseti, mwana wa Sauli, aliyekuwa mchukivu wako, aliyeitaka roho yako. Siku hii ya leo Bwana amempatia bwana wangu malipizi kwake Sauli na kwa kizazi chake. Ndipo, Dawidi alimpomjibu Rekabu na ndugu yake Baana, wana wa Rimoni wa Beroti, akiwaambia: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyeikomboa roho yangu katika masongano yote, nilimkamata yule aliyeniletea habari ya kwamba: Tazama, Sauli amekufa! Naye alijiwazia kuwa mwenye habari njema, lakini nikamwua huko Siklagi kuwa mshahara, niliompa wa habari zake. Nanyi m wabaya zaidi wasiomcha Mungu mlipomwua mtu mwongofu nyumbani mwake, akiwa amelala kitandani pake. Sasa itakuwaje? Sitailipiza damu yake mikononi mwenu na kuwang'oa katika nchi? Kisha Dawidi akawaagiza vijana wake, wakawaua, kisha wakawakata mikono na miguu, wakawatungika penye ziwa la Heburoni. Nacho kichwa cha Isiboseti wakakichukua, wakakizika kaburini kwa Abineri kule Heburoni. Mashina yote ya Waisiraeli wakaja Heburoni kwake Dawidi, wakamwambia kwamba: Tazama, sisi na wewe tu mifupa ya mmoja, nazo nyama za miili yetu ni za mmoja. Napo hapo kale, Sauli alipokuwa mfalme wetu bado, aliyewaongoza Waisiraeli kwenda na kurudi vitani ni wewe, naye Bwana alikuambia: Wewe utawachunga walio ukoo wangu wa Waisiraeli, nawe wewe utawatawala Waisiraeli. Wazee wote wa Waisiraeli wakamjia mfalme huko Heburoni, mfalme Dawidi akafanya agano nao huko Heburoni mbele ya Bwana, wakampaka Dawidi mafuta, awe mfalme wao Waisiraeli. Dawidi alikuwa mwenye miaka 30 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 40. Huko Heburoni alikuwa mfalme wa Wayuda miaka 7 na miezi 6, namo Yerusalemu alikuwa mfalme wa Waisiraeli na wa Wayuda wote miaka 33. Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kwa Wayebusi waliokuwa bado wenyeji wa nchi hiyo, nao wakamwambia Dawidi kwamba: Humu hutaiangia kabisa usipowaondoa vipofu na viwete, ni kwamba: Dawidi hataingia humu. Lakini Dawidi akaliteka boma la Sioni, ndio mji wa Dawidi. Siku hiyo Dawidi alisema: Kila anayetaka kuwapiga Wayebusi na ashike njia ya kukwea katika mfereji, awafikie wale viwete na vipofu wanaochukizwa na roho yake Dawidi. Kwa hiyo husema fumbo la kwamba: Kipofu au kiwete alipo, mtu haingii nyumbani. Dawidi akakaa mle bomani, akaliita mji wa Dawidi, Dawidi akaujenga pande zote kuanzia Milo mpaka hapo penye nyumba za mji. Dawidi akaendelea kuwa mkuu, kwa sababu Bwana Mungu mwenye vikosi alikuwa naye. Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Dawidi na miti ya miangati na maseremala na waashi wa kujenga na mawe, wakamjengea Dawidi nyumba. Ndipo, Dawidi alipojua, ya kuwa Bwana amemweka kweli kuwa mfalme wao Waisiraeli, kwani ufalme wake ukaja kutukuka zaidi kwa ajili ya ukoo wake wa Waisiraeli. Kisha Dawidi akachukua tena masuria na wake mle Yerusalemu alipokwisha kuingia humo na kutoka Heburoni, Dawidi akazaa tena wana wa kiume na wa kike. Haya ndiyo majina ya wana, waliozaliwa mle Yerusalemu: Samua na Sobabu na Natani na Salomo, na Ibuhari na Elisua na Nefegi na Yafia, na Elisama na Eliada na Elifeleti. Wafilisti waliposikia, ya kuwa wamempaka Dawidi mafuta, awe mfalme wa Waisiraeli, ndipo, Wafilisti wote walipopanda kumtafuta Dawidi. Dawidi alipovisikia, akashuka kuja ngomeni. Wafilisti wakaja, wakajieneza Bondeni kwa Majitu. Dawidi akamwuliza Bwana kwamba: Nikipanda kupigana na Wafilisti, utawatia mkononi mwangu? Bwana akamwambia Dawidi: Panda! Kwani nitawatia Wafilisti mkononi mwako. Ndipo, Dawidi alipokuja Baali-Perasimu; Dawidi alipowapiga huko akasema: Bwana amewaatua adui zangu mbele yangu, kama maji yanavyoatua ukingo. Kwa sababu hii akapaita mahali pale jina lake Baali-Perasimu (Maatuko). Wakaacha kule vinyago vyao, lakini Dawidi na watu wake wakavichukua. Lakini Wafilisti wakapanda tena, wakajieneza kulekule Bondeni kwa Majitu. Naye Dawidi alipomwuliza Bwana, akamwambia: Usipande, ila uzunguke migongoni kwao, upate kuwajia ukitoka juu, misandarusi iliko. Hapo, utakaposikia vileleni kwa misandarusi shindo kama ya watu wapitao, basi, hapo piga mbio! Kwani ndipo, Bwana atakapotokea, akutangulie kuyapiga majeshi ya Wafilisti. Dawidi akafanya, kama Bwana alivyomwagiza, akawapiga Wafilisti toka Geba, hata mtu afike Gezeri. Dawidi akawakusanya tena wapiga vita wote waliochaguliwa kwao Waisiraeli, watu 30000. Kisha Dawidi akaondoka, akaenda nao hao watu wote waliokuwa naye kwenda Bale wa Yuda kulichukua huko Sanduku la Mungu lililoitwa jina lake kwa Jina la Bwana Mwenye vikosi akaaye juu ya Makerubi. Wakalipandisha Sanduku la Mungu katika gari jipya wakilitoa katika nyumba ya Abinadabu iliyokuwa kilimani juu; nao Uza na Ayo, wana wa Abinadabu, wakaliendesha hilo gari jipya. Walipokwisha kulitoa katika nyumba ya Abinadabu iliyokuwa kilimani juu, wakalipeleka Sanduku la Mungu, Ayo akilitangulia Sanduku. Dawidi mwenyewe nao watu walio wa mlango wa Isiraeli wakalitangulia na kucheza mbele ya Bwana na kupiga vyombo vyote vya kuchezea vilivyotengenezwa kwa mivinje kama mazeze na mapango na patu na njuga na matoazi. Walipofika pake Nakoni pa kupuria, Uza akalipelekea Sanduku la Mungu mkono, alishike, kwa kuwa ng'ombe walijikwaa. Ndipo, makali ya Bwana yalipomwakia Uza, naye Mungu akampiga huko kwa ajili ya hilo kosa, akafa papo hapo penye Sanduku la Mungu. Hapo Dawidi akaingiwa na uchungu, ya kuwa Bwana amempiga Uza pigo kama hilo, wakapaita mahali pale Peresi-Uza (Pigo la Uza) mpaka siku hii ya leo. Siku hiyo Dawidi akashikwa na woga wa kumwogopa Bwana kwamba: Sanduku la Bwana litawezaje kufika kwangu? Kwa hiyo Dawidi hakutaka kuliingiza Sanduku la Bwana kwake mjini kwa Dawidi, Dawidi akashika njia nyingine, akaliweka nyumbani mwa Obedi-Edomu wa Gati. Humo nyumbani mwa Obedi-Edomu wa Gati Sanduku la Bwana likakaa miezi mitatu, naye Bwana akambariki Obedi-Edomu na mlango wake wote. Mfalme Dawidi alipopashwa habari kwamba: Bwana ameubariki mlango wa Obedi-Edomu nayo yote yaliyo yake kwa ajili ya Sanduku la Mungu, Dawidi akaenda, akalitoa Sanduku la Mungu nyumbani mwa Obedi-Edomu, akalipandisha mjini kwa Dawidi kwa furaha. Ikawa, wao wachukuzi wa Sanduku la Bwana walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja ng'ombe ya tambiko na ndama aliyenona. Dawidi akawa akicheza kwa nguvu zote mbele ya Bwana, naye Dawidi alikuwa amevaa kisibau cheupe cha ukonge. Ndivyo, Dawidi na mlango wote wa Waisiraeli walivyolipandisha Sanduku la Bwana kwa kushangilia na kupiga mabaragumu. Ikawa, Sanduku la Bwana lilipoingia mjini kwa Dawidi, Mikali, binti Sauli, alichungulia dirishani; naye alipomwona mfalme Dawidi, alivyorukaruka na kuchezacheza mbele ya Bwana, ndipo, alipombeza moyoni mwake. Walipokwisha kuliingiza Sanduku la Bwana wakaliweka mahali pake katikati ya lile hema, Dawidi alilolipigia. Kisha Dawidi akamtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kumshukuru. Dawidi alipokwisha kuzitoa hizo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani akawabariki watu katika Jina la Bwana Mwenye vikosi. Kisha akawagawia watu wote wa huo mkutano wote wa Waisiraeli, waume kwa wake, kila mtu kipande kimoja cha mkate na kipande kimoja cha nyama na andazi moja la zabibu, kisha watu wote wakaenda zao kila mtu nyumbani kwake. Dawidi naye aliporudi kuwabariki walio wa mlango wake, Mikali, binti Sauli, akamwendea Dawidi njiani, akasema: Kweli leo mfalme wa Waisiraeli amejitukuza alipojivua nguo machoni pa vijakazi wa watumishi wake, kama mmoja wao walio wa ovyoovyo tu anavyojivika uchi. Lakini Dawidi akamwambia Mikali: Bwana ndiye aliyenichagua na kumwacha baba yako na mlango wake wote, aliponiagiza mimi kuwa mkuu wao walio ukoo wake Bwana nao wao Waisiraeli, naye yeye Bwana ndiye, ambaye ninataka kucheza mbele yake. Tena ninataka kujipunguza kupapita hapo pa leo, niwe mnyenyekevu machoni pangu mwenyewe; ndivyo, nitakavyojipatia utukufu kwao vijakazi, uliowasema. Lakini Mikali, binti Sauli, hakuwa na mwana mpaka siku hiyo, alipokufa. Ikawa, mfalme alipokaa nyumbani mwake, kwa kuwa Bwana alikuwa amemtuliza akiwanyamazisha adui zake zote waliomzunguka, ndipo, mfalme alipomwambia mfumbuaji Natani: Tazama, mimi ninakaa katika nyumba iliyojengwa kwa miangati, lakini Sanduku la Mungu linakaa katika mapazia tu. Natani akamwambia mfalme: Yote yaliyomo moyoni mwako nenda, uyafanye! Kwani Bwana yuko pamoja na wewe. Lakini usiku uleule neno la Bwana likamjia Natani kwamba: Nenda, umwambie mtumishi wangu Dawidi: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Wewe unijengee nyumba, nikae? Kwani sikukaa nyumbani tangu siku ile, nilipowatoa wana wa Isiraeli huko Misri nikiwaleta huku, mpaka siku hii ya leo, nikawa nikienda na kukaa katika hema lililokuwa Kao langu. Je? Hapo pote, nilipokwenda pamoja na wana wote wa Isiraeli, nilimwambia hata mmoja wao wa mashina ya Waisiraeli, niliowaagiza kuwachunga walio ukoo wangu wa Waisiraeli, na kumwuliza neno la kwamba: Mbona hamnijengei nyumba ya miangati? Kwa hiyo umwambie sasa mtumishi wangu Dawidi: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mimi nilikuchukua malishoni, ulipowafuata kondoo, uwe mwenye kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli. Nikawa pamoja na wewe po pote, ulipokwenda, nikawaangamiza adui zako wote mbele yako; nitakupatia jina kubwa lililo sawa na majina ya wakubwa walioko huku nchini. Nao walio ukoo wangu wa Waisiraeli nitawapatia mahali, nitakapowapanda, wapate kukaa hapo pasipo kuhangaika tena, wala watu waovu wasiwakorofishe tena kama huko kwanza tangu siku zile, nilipowaagiza waamuzi, wawatawale walio ukoo wangu wa Waisiraeli. Lakini wewe nitakupa kutulia nikiwanyamazisha adui zako wote, nawe wewe Bwana anakupasha habari, ya kuwa yeye Bwana atakutengenezea nyumba. Kwani siku zako zitakapotimia, uende kulala pamoja na baba zako, ndipo, nitakapoinua nyuma yako mzao wako atakayetoka mwilini mwako, niusimike ufalme wake. Yeye ndiye atakayelijengea Jina langu nyumba, nami nitakisimamisha kiti cha ufalme wake, kipate kuwapo kale na kale. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; atakapofanya kiovu, nitamchapa kwa fimbo ya kiwatu na kwa mapigo yapasayo wana wa watu. Lakini upole wangu hautaondoka kwake, kama nilivyouondoa kwake Sauli, nilipomwondoa usoni pako. Mlango wako na ufalme wako utakuwa umeshupaa kale na kale machoni pako, nacho kiti chako cha kifalme kitakuwa kimesimamishwa kale na kale. *Natani akamwambia Dawidi haya maneno yote sawasawa, kama alivyoambiwa mwenyewe na kuonyeshwa. Kisha mfalme Dawidi akaingia pake Bwana, akakaa hapo akisema: Bwana Mungu, mimi ni nani? nao mlango wangu ni nini, ukinileta, nifike hapa? Lakini hayo yakawa madogo machoni pako, Bwana Mungu, kwa hiyo umeyasema yatakayoujia mlango wa mtumishi wako katika siku zilizo mbali bado, hayo nayo umeyasema kimtu, Bwana Mungu. Dawidi akuambie nini tena? Maana wewe unamjua mtumishi wako, Bwana Mungu. Kwa ajili ya Neno lako na kwa mapenzi ya moyo wako umeyafanya hayo makubwa yote, umjulishe mtumishi wako. Kwa hiyo u mkubwa, Bwana Mungu, kwani hakuna anayefanana na wewe, hakuna Mungu, asipokuwa wewe, kwa hayo yote, tuliyoyasikia kwa masikio yetu. Tena liko taifa moja tu huku nchini linalofanana na ukoo wako wa Waisiraeli? Hao ndio, Mungu aliokwenda kuwakomboa, wawe ukoo wake, ajipatie Jina kwa kufanya kwao katika nchi yako matendo makubwa yanayoogopesha, ulipofukuza wamizimu na miungu yao mbele yao walio ukoo wako, uliowakomboa, wawe wako, ulipowatoa huko Misri. Ukajiwekea ukoo wako wa Waisiraeli kuwa ukoo wako kale na kale, wewe Bwana ukawa Mungu wao. Sasa, Bwana Mungu, neno hilo, ulilolisema la mtumishi wako na la mlango wake, lisimamishe kuwapo kale na kale ukifanya, kama ulivyosema! Ndivyo, Jina lako litakavyokuwa kubwa kale na kale kwamba: Bwana Mwenye vikosi ni Mungu wa Isiraeli, tena ndivyo, mlango wa mtumishi wako Dawidi utakavyokuwa wenye nguvu mbele yako. Kwani wewe Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, umelifunua sikio la mtumishi wako, asikie ya kwamba: Mimi nitakujengea nyumba. Kwa hiyo mtumishi wako amejipa moyo wa kukuomba maombo haya. Sasa Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu; kwa hiyo maneno yako yatatimia kweli, hayo mema, uliyomwambia mtumishi wako, yapate kuwa. Sasa na ikupendeze kuubariki mlango wa mtumishi wako, uwepo kale na kale usoni pako! Kwani wewe, Bwana Mungu, umeyasema; kwa hiyo mlango wa mtumishi wako utakuwa umebarikiwa kale na kale kwa kuipata mbaraka yako.* Hayo yalipokwisha, Dawidi akawapiga Wafilisti, akawashinda; kisha Dawidi akaishika mwenyewe hatamu ya mji mkuu, isishikwe tena na Wafilisti. Nao Wamoabu akawapiga, akawapima kwa kamba akiwalaza chini, akapima hivyo: wa kamba mbili wakawa wa kuuawa, nao wote wa kamba moja wakawa wa kuachwa uzimani; nao Wamoabu wakawa watumishi wa Dawidi, wakamletea mahongo. Kisha Dawidi akampiga Hadadezeri, mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kuusimika tena ufalme wake huko kwenye jito la Furati. Dawidi akateka kwake wapanda farasi 1700 na askari waliokwenda kwa miguu 20000, nao farasi wote wa kuvuta magari Dawidi akawakata mishipa, akajisazia farasi wa magari mia tu. Washami Wa Damasko walipokuja kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Dawidi akapiga kwao Washami watu 22000. Dawidi akaweka askari kwao Washami wa Damasko, hao Washami wakawa watumishi wa Dawidi, wakamletea mahongo, ndivyo, Bwana alivyompa Dawidi kushinda po pote, alipokwenda. Dawidi akazichukua ngao za dhahabu, watumishi wa Hadadezeri walizokuwa nazo, akazipeleka Yerusalemu. Namo mle Beta na Berotai iliyokuwa miji ya Hadadezeri Dawidi akachukua shaba nyekundu nyingi mno. Toi, mfalme wa Hamati, aliposikia, ya kuwa Dawidi amevipiga vikosi vyote vya Hadadezeri, Toi akamtuma mwanawe Yoramu kwake mfalme Dawidi kumpongeza na kumbariki, kwa kuwa amepigana na Hadadezeri na kumshinda, kwani Toi na Hadadezeri walikuwa wakipigana vita, naye akampelekea mkononi mwake vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu na vyombo vya shaba. Hivi navyo mfalme Dawidi akavitakasa kuwa mali za Bwana, kama alivyozitakasa nazo fedha na dhahabu, alizozichukua kwa mataifa yote, aliyoyashinda, kama kwao Washami na Wamoabu na wana wa Amoni na Wafilisti na Waamaleki, hata nyara za Hadadezeri, mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba. Dawidi aliporudi kwa kuwapiga Washami akajipatia jina kuu kwa kuua watu 18000 Bondeni kwa Chumvi. Kisha Dawidi akaweka askari kwa Waedomu, kwao Waedomu akaweka askari po pote, nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Dawidi. Ndivyo, Bwana alivyompa Dawidi kushinda po pote, alipokwenda. Dawidi akawa mfalme wa Waisiraeli wote, naye Dawidi akawatengenezea watu wake wote mashauri yaliyokuwa sawa, maana yaliongoka. Naye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa vikosi, naye Yosafati, mwana wa Ahiludi, alikuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa. Naye Sadoki, mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki, mwana wa Abiatari, walikuwa watambikaji, naye Seraya alikuwa mwandishi. Naye Benaya, mwana wa Yoyada, alikuwa mkuu wao Wakreti na Wapuleti, nao wana wa Dawidi walikuwa watambikaji. Dawidi akauliza: Yuko bado aliyesalia wa mlango wa Sauli, nimgawie mema kwa ajili yake Yonatani? Kulikuwako mtumishi wa nyumbani mwa Sauli, jina lake Siba; wakamwita, aje kwa Dawidi, naye mfalme akamwuliza: Wewe ndiwe Siba? Akasema: Ndimi mtumishi wako. Mfalme akamwuliza: Yuko bado mtu wa mlango wa Sauli, nimgawie mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme: Yuko bado mwana wa Yonatani, naye amelemaa miguu. Mfalme akamwuliza: Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme: Tazama, yumo nyumbani mwa Makiri, mwana wa Amieli, huko Lo-Debari. Ndipo, mfalme Dawidi alipotuma watu kumchukua nyumbani mwa Makiri, mwana wa Amieli, huko Lo-Debari. Mefiboseti, mwana wa Yonatani, mwana wa Sauli, alipofika kwake Dawidi akajiangusha usone pake kumwangukia; Dawidi akasema: Mefiboseti! Naye akasema: Mimi hapa mtumwa wako. Dawidi akamwambia: Usiogope! Kwani mimi nitakugawia mema kwa ajili ya baba yako Yonatani, nitakurudishia mashamba yote ya babu yako Sauli, tena wewe utakula chakula siku zote mezani pangu. Ndipo, alipomwangukia akisema: Mimi, mtumwa wako, ni nani, ukijielekeza kumtazama mbwa mfu, kama mimi nilivyo? Kisha Dawidi akamwita Siba, yule kijana wa Sauli, akamwambia: Yote yaliyokuwa mali zake Sauli na za mlango wake wote nimempa huyu mwana wa bwana wako. Nawe utamlimia shamba, wewe na wanao na watumishi wako, tena utamvunia mazao ya shambani, yawe chakula cha mwana wa bwana wako, ayale. Tena Mefiboseti, mwana wa bwana wako, atakula chakula siku zote mezani pangu. Naye Siba alikuwa mwenye wana 15 na watumishi 20. Siba akamwambia mfalme: Yote, bwana wangu mfalme anayomwagiza mtumwa wake, mtumwa wako atayafanya vivyo hivyo. Kwa hiyo Mefiboseti akawa akila mezani pa Dawidi kama mmoja wao wana wa mfalme. Naye Mefiboseti alikuwa na mwana mdogo, jina lake Mika, nao wote waliokaa nyumbani mwa Siba walikuwa watumishi wake Mefiboseti. Naye Mefiboseti akawa akikaa Yerusalemu, kwani alikuwa akila siku zote mezani pa mfalme, naye alikuwa amelemaa miguu yote miwili. Hayo yalipokwisha, akafa mfalme wa wana wa Amoni, naye mwanawe Hanuni akawa mfalme mahali pake. Dawidi akasema: Nitamfanyizia Hanuni, mwana wa Nahasi, mambo ya upole, kama baba yake alivyonifanyizia nami mambo ya upole. Kwa hiyo Dawidi akatuma wajumbe, wamtulize moyo kwa ajili ya baba yake. Lakini watumishi wa Dawidi walipofika katika nchi ya wana wa Amoni, wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia bwana wao Hanuni; Je? Dawidi anataka kweli kumheshimu baba yako machoni pako akituma kwako wajumbe wa kukutuliza moyo? Dawidi hakuwatuma watumishi wake kwako kuuchunguza mji huu na kuupeleleza, apate kuufudikiza? Ndipo, Hanuni alipowakamata watumishi wa Dawidi, akawanyoa nusu ya ndevu zao, akawakatia mavazi yao nusu kuyafikisha matako yao, kisha akawapa ruhusa kwenda zao. Watu walipompasha Dawidi habari hizo, akatuma wengine kuwaendea njiani, kwa kuwa watu hawa walikuwa wametwezwa sana; mfalme akawaambia: Kaeni Yeriko, mpaka ndevu zenu zikue tena, kisha rudini! Wana wa Amoni walipoona, ya kuwa wamejichukizisha kwake Dawidi, ndipo, wana wa Amoni walipotuma watu kuwakodisha Washami wa Beti-Rehobu na Washami wa Soba, ni askari waliokwenda kwa miguu 20000, tena mfalme wa Maka na watu 1000 na watu 12000 wa Tobu. Dawidi alipoyasikia akamtuma Yoabu na vikosi vyote vya mafundi wa vita. Wana wa Amoni wakatoka, wakajipanga penye lango la mji, wapige vita, nao Washami wa Soba na wa Rehobu na watu wa Tobu na wa Maka wakawa peke yao shambani. Yoabu alipoona, ya kuwa wamejipanga kupiga vita usoni na mgongoni pake, akachagua wengie katika wateule wote wa Waisiraeli, akawapanga, wapigane na Washami. Nao watu waliosalia akawatia mkononi mwa ndugu yake Abisai, akawapanga, wapigane na wana wa Amoni, akasema: Kama Washami wanapata nguvu za kunishinda, sharti uje kunisaidia. Tena kama wana wa Amoni wanapata nguvu za kukushinda, sharti nije, nikusaidie. Jipe moyo, tushikizane mioyo, tuwapiganie watu wa kwetu na miji ya Mungu wetu! Ndipo, Bwana atakapoyafanya, aliyoyaona kuwa mema. Kisha Yoabu na watu wake, aliokuwa nao, wakawasogelea Washami kupigana nao, lakini wao wakawakimbia. Wana wa Amoni walipoona, ya kuwa Washami wamekimbia, ndipo, nao walipomkimbia Abisai, wakaigia mjini mwao, lakini Yoabu akarudi akitoka kwa wana wa Amoni, akaja Yerusalemu. Washami walipoona, ya kuwa wameshindwa nao Waisiraeli, wakakusanyika pamoja. Kisha Hadadezeri akatuma watu kuwachukua Washami walioko ng'ambo ya huko ya jito hilo; nao wakaja Helamu, naye mkuu wa vikosi vya Hadadezeri, jina lake Sobaki, akawaongoza. Dawidi alipopashwa habari hizi, akawakusanya Waisiraeli wote, akauvuka Yordani, akaja Helamu; ndipo, Washami walipojipanga kukutana na Dawidi, wakapigana naye. Kisha Washami wakawakimbia Waisiraeli, Dawidi akaua kwao Washami farasi waliovuta magari 700 na wapanda farasi 40000, hata Sobaki, mkuu wa vikosi vyao, akampiga, naye akafa papo hapo. Wafalme wote waliomtumikia Hadadezeri walipoona, ya kuwa wameshindwa na Waisiraeli, wakafanya mapatano na Waisiraeli, wakawatumikia. Kwa hiyo Washami wakaogopa kuwasaidia wana wa Amoni tena. Ikawa, mwaka ulipopita, siku hizo wafalme wanapozoea kwenda vitani, ndipo, Dawidi alipomtuma Yoabu na watumishi wake pamoja naye na Waisiraeli wote, wakawaangamiza wana wa Amoni, wakausonga mji wa Raba kwa kuuzinga, lakini Dawidi alikuwa anakaa Yerusalemu. Siku moja saa za jioni Dawidi akaondoka kitandani pake, akatembea darini juu ya nyumba ya mfalme. Toka huko juu darini akaona mwanamke aliyeoga, naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana wa kumtazama. Dawidi akatuma mtu kuuliza, huyo mwanamke kama ni wa nani, akaambiwa: Huyo siye Bati-Seba, binti Eliamu, mkewe Mhiti Uria? Kisha Dawidi akatuma wajumbe, akamchukua; alipofika kwake, akalala naye. Naye huyu alipokwisha kujieua kwa ajili ya huo uchafu wake akarudi nyumbani mwake. Huyu mwanamke alipopata mimba akatuma kumpasha Dawidi habari kwamba: Mimi ni mwenye mimba. Ndipo, Dawidi alipotuma kwa Yoabu kwamba: Mtume Mhiti Uria, aje kwangu! Naye Yoabu akamtuma Uria kwake Dawidi. Uria alipofika kwake Dawidi akamwuliza, kama Yoabu hajambo, kama watu hawajambo, tena jinsi vita vinavyoendelea. Kisha Dawidi akamwambia Uria: Shuka kwenda nyumbani mwako kuiosha miguu yako! Uria alipotoka nyumbani mwa mfalme, chakula cha kifalme kikatoka nacho kumfuata. Lakini Uria akalala mlangoni penye nyumba ya mfalme pamoja na watumishi wote wa bwana wake, hakushuka kwenda nyumbani mwake. Watu walipompasha Dawidi habari hizo kwamba: Uria hakushuka kwenda nyumbani mwake, Dawidi akamwuliza Uria: Je? Hukutoka njiani? Mbona hushuki kwenda nyumbani mwako? Ndipo, Uria alipomwambia Dawidi: Lile Sanduku na Waisiraeli na Wayuda wanakaa vibandani; naye bwana wangu Yoabu na watumishi wa bwana wangu wanalala porini; basi, mimi nitawezaje kuingia nyumbani mwangu, nile, ninywe, kisha nilale na mke wangu? Hivyo, ulivyo mzima, tena hivyo, roho yako ilivyo nzima, sitafanya kabisa jambo kama hilo. Dawidi akamwambia Uria: Kaa huku hata leo! Kesho nitakupa ruhusa, uende zako. Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku hiyo. Kesho yake, Dawidi alipomwita, akala, akanywa kwake; ndipo, alipomlewesha. Jioni akatoka kulala penye kilalo chake pamoja na watumishi wa bwana wake, asishuke kwenda nyumbani mwake. Kulipokucha, Dawidi akamwandikia Yoabu barua, akaipeleka mkononi mwa Uria. Namo katika barua ameandika kwamba: Mwekeni Uria mahali pa mbele, mapigano yanapozidi kuwa makali! Kisha rudini nyuma na kumwacha, apigwe, afe! Yoabu alipoyaangalia mambo ya huo mji, akamweka Uria mahali, alipopajua, ya kuwa hapo watatokea watu wenye nguvu. Watu wa huo mji walipotoka kupigana na Yoabu, wakauawa watu miongoni mwao walio watu wake na watumishi wa Dawidi, hata yule Mhiti Uria akafa naye. Kisha Yoabu akatuma kumpasha Dawidi habari za mambo yote ya vita. Akamwagiza yule mjumbe kwamba: Utakapokwisha kumwambia mfalme habari zote za vita, labda machafuko yatampata mfalme, akuulize: Mbona mmeukaribia huo mji kupigana nao? Hamkujua, ya kuwa watapiga mishale toka juu ukutani? Ni nani aliyempiga Abimeleki, mwana wa Yerubeseti? Siye mwanamke aliyemtupia jiwe la sago toka juu ukutani, afe huko Tebesi? Mbona mmeukaribia mji hivyo? Basi, ndipo, utakapomwambia: Hata mtumishi wako yule Mhiti Uria, amekufa naye. Kisha yule mjumbe akaenda, akaja kumpasha Dawidi habari hizo zote, Yoabu alizomtuma. Huyo mjumbe akamwambia Dawidi: Wale watu wakatutolea nguvu na kututokea kwetu porini, nasi tukawaendea hata hapo pa kuliingilia lango la mji. Ndipo, wapiga mishale walipowapiga watumishi wako toka juu ukutani, watu wakafa miongoni mwa watumishi wa mfalme, hata mtumishi wako, yule Mhiti Uria, akafa. Naye Dawidi akamwambia huyo mjumbe: Hivyo umwambie Yoabu: Jambo hili lisiwe baya machoni pako! Kwani upanga hula huku na huko; jipe moyo, upigane na huo mji, mpaka uubomoe! Hivyo ndivyo, umshikize moyo. Mkewe Uria aliposikia, ya kuwa mumewe Uria amekufa, akamwombolezea bwana wake. Siku za matanga zilipopita, Dawidi akatuma kumchukua nyumbani mwake, akawa mkewe, akamzalia mwana. Lakini jambo hili, Dawidi alilolifanya, likawa baya machoni pake Bwana. Bwana akamtuma Natani kwenda kwake Dawidi. Alipofika kwake akamwambia: Kulikuwa na watu wawili, wamekaa katika mji mmoja, mmoja ni mkwasi, mmoja ni maskini. Yule mkwasi alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi mno. Lakini yule maskini alikuwa hanacho cho chote, kisipokuwa kikondoo kimoja tu, alichokinunua. Akakifuga, kikakua nyumbani mwake pamoja na watoto wake, kikala chakula chake, kikanywa katika kikombe chake mwenyewe, kikalala kifuani pake, maana kilikuwa kama mtoto wake wa kike. Siku moja yule mkwasi akafikiwa na mgeni, akaona uchungu wa kuchukua kondoo wake au ng'ombe wake mmoja wa kumpa yule mpitaji aliyefikia kwake, basi, akakichukua kikondoo cha yule maskini, akamtengenezea yule mtu aliyefikia kwake. Ndipo, makali ya Dawidi yalipowaka moto sana kwa ajili ya mtu huyo, akamwambia Natani: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, mtu aliyeyafaya hayo ni mtu wa kufa! Kile kikondoo nacho sharti akilipe mara nne, kwa kuwa amefanya jambo kama hilo pasipo kuona huruma. Natani akamwambia Dawidi: Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mimi nilikupaka mafuta, uwe mfalme wa Waisiraeli. Mimi nami nikakuponya mkononi mwa Sauli, nikakupa nyumba ya bwana wako nao wanawake wa bwana wako, ulale nao, nikakupa nayo milango ya Isiraeli na ya Yuda; kama haya ni machache, nitayaongeza na kukupa haya na haya. Kwa sababu gani umelibeza neno la Bwana ukilifanya lililo baya machoni pake? Yule Mhiti Uria umemwua kwa upanga, ukamchukua mkewe, awe mke wako, ulipokwisha kumwua kwa panga za wana wa Amoni. Sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako kale na kale, kwa kuwa umenibeza na kumchukua mkewe yule Mhiti Uria, awe mke wako. Hivi ndivyo, anavyosema Bwana: Utaniona nikikupatia jambo baya litakalotoka nyumbani mwako, nitawachukua wake zako machoni pako, nimpe mwenzako, alale nao wake zako katika mwanga wa jua hili. Kweli umelifanya jambo lako na kufichaficha, lakini mimi nitalifanya jambo hilo mbele ya Waisiraeli wote na mbele ya jua. Ndipo, Dawidi alipomwambia Natani: Nimemkosea Bwana! Natani akamwambia Dawidi: Kwa hiyo Bwana ameliondoa hili kosa lako, hutakufa. Lakini kwa kuwa umewapatia wachukivu wa Bwana katika jambo hilo sababu ya kuyaongeza mabezo yao, yule mwana aliyezaliwa hana budi kufa. Natani alipokwisha akwenda nyumbani kwake, Bwana akampiga yule mtoto, mkewe Uria aliyemzalia Dawidi, akawa mgonjwa sana. Dawidi akamtafuta Mungu na kumwombea mtoto, kisha Dawidi akafunga, tena alipoingia mwake akalala chini usiku kucha. Wazee wa nyumbani mwake wakamtokea, wamwinue chini, lakini akakataa, nacho chakula hakula nao. Ilipokuwa siku ya saba, mtoto akafa; nao watumishi wa Dawidi wakaogopa kumpasha habari hii, ya kuwa mtoto amekufa, kwani waliwaza kwamba: Mtoto alipokuwa angali akiishi, hakuzisikia sauti zetu, tulipomwambia neno; sasa tutawezaje kumwambia: Mtoto amekufa? Angejifanyia kibaya. Lakini Dawidi alipowaona watumishi wake, wakinong'onezana, Dawidi akatambua, ya kuwa mtoto amekufa; kwa hiyo Dawidi akawauliza watumishi wake: Mtoto amekufa? wakamwambia: Amekufa. Ndipo, Dawidi alipoondoka chini, akaoga na kujipaka mafuta, akavaa nguo nyingine, akaingia nyumbani mwa Bwana, akamwangukia. Kisha akaingia nyumbani mwake na kutaka vyakula; walipokwisha kumwandalia, akala. Ndipo, watumishi wake walipomwuliza: Jambo hili, unalolifanya, linakuwaje? Kwani mtoto alipokuwa angali akiishi, umefunga na kulia machozi; lakini mtoto alipokwisha kufa, umeinuka, ukala chakula. Akasema: Kweli mtoto alipokuwa angali akiishi, nimefunga na kulia machozi, kwani nilisema: Labda Bwana atanihurumia, mtoto apate kupona. Lakini sasa amekwisha kufa, nifungeje tena? Nitaweza kumrudisha uzimani tena? Mimi nitakwenda kwake, lakini yeye harudi kwangu. Dawidi akamtuliza moyo mkewe Bati-Seba, akaingia kwake, akalala naye, kisha akazaa mtoto mume, akamwita jina lake Salomo (Mtulivu), naye Bwana akampenda. Baadaye Dawidi akampeleka, akamtia mkononi mwa mfumbuaji Natani, huyo akamwita jina lake Yedidia (Mpendwa wa Bwana) kwa ajili ya Bwana. Yoabu akapiga vita kule Raba kwa wana wa Amoni, akauteka huo mji wa kifalme. Ndipo, Yoabu alipotuma wajumbe kwake Dawidi kwamba: Nimepiga vita huku Raba, nikauteka mji huu ulio wenye maji. Sasa wakusanye watu waliosalia, uuzinge mji huu, uuteke, nisiuteke mimi mji huu, jina langu likitangazwa humu. Ndipo, Dawidi alipowakusanya watu wote, akaenda nao Raba, akapiga vita huko, akauteka. Akaliondoa taji la mfalme kichwani pake, nao uzito wake ulikuwa frasila tatu za dhahabu, nalo lilikuwa na vito vyenye kima; hilo Dawidi akavikwa kichwani. Namo mjini akatoa mateka mengi sana. Nao watu waliokuwamo akawatoa, akawaweka chini ya misumeno na chini ya magari ya chuma ya kupuria na chini ya mashoka ya chuma, wengine akawashurutisha kupita katika moto wa tanuru. Hivyo Dawidi akaifanyizia miji yote ya wana wa Amoni. Kisha Dawidi akarudi Yerusalemu pamoja na watu wake wote. Hayo yalipokwisha kufanyika, Abisalomu, mwana wa Dawidi, alikuwa na umbu lake, jina lake Tamari, naye alikuwa mzuri; kwa hiyo Amunoni, mwana wa Dawidi, akampenda. Naye Amunoni akasongeka moyoni, akapata kuwa mgonjwa kwa ajili ya umbu lake Tamari, kwani alikuwa mwanamwali, naye Amunoni akaviona kuwa vigumu sana kumfanyizia lo lote. Lakini Amunoni alikuwa na mwenzake, jina lake Yonadabu, mwana wa Simea, kaka yake Dawidi; huyu Yonadabu alikuwa mwerevu sana. Huyu akamwuliza: Mbona wewe, mwana wa mfalme, unanyongeka hivyo kila kunapokucha? Huwezi kunisimulia sababu yake? Ndipo, Amunoni alipomwambia: Mimi nampenda Tamari, umbu lake ndugu yangu Abisalomu. Yonadabu akamwambia: Lala kitandani pako kuwa kama mgonjwa sana! Kisha baba yako akija kukutazama, umwambie: Kama umbu langu Tamari angekuja kuniandalia chakula na kukitengeneza hicho chakula machoni pangu, nipate kuviona, basi, ningekula na kuvipokea mkononi mwake. Kwa hiyo Amunoni akalala kitandani kuwa kama mgonjwa. Mfalme alipokuja kumtazama, Amunoni akamwambia mfalme: Kama umbu langu Tamari angekuja kuandalia machoni pangu vikate viwili, ningevila na kuvipokea mkononi mwake. Ndipo, Dawidi alipomtuma Tamari kwenda mle nyumbani kwamba: Nenda nyumbani mwa umbu lako Amunoni, umtengenezee chakula! Ndipo, Tamari alipokwenda nyumbani mwa umbu lake Amunoni, naye alikuwa amelala; akachukua unga, akaukanda, akautengeneza machoni pake kuwa vikate, akavioka hivyo vikate. Kisha akakichukua kikaango, akavitia katika sahani machoni pake, lakini Amunoni akakataa kuvila, akasema: Watoeni watu wote humu mwangu! Walipokwisha kuwatoa watu wote mwake, Amunoni akamwambia Tamari: Kilete hicho chakula chumbani humu, nikile na kukipokea mkononi mwako! Tamari akavichukua hivyo vikate, alivyovitengeneza, akampelekea umbu lake Amunoni mle chumbani. Alipompa, avile, akamshika na kumwambia: Njoo, umbu langu, ulale kwangu! Lakini akamwambia: Sivyo, umbu langu, usinichukue kwa nguvu. Kwani mambo kama hayo hayafanywi kwao Waisiraeli, nawe usiufanye upumbavu huu! Mimi nami nitakwenda wapi nikitwezwa hivyo? Wewe nawe utakuwa mpumbavu mwenzao walio hivyo kwao Waisiraeli. Ila sema na mfalme sasa, kwani hatakukataza kunioa. Lakini hakutaka kuyasikia, aliyomwambia, akamkamata kwa nguvu na kumshurutiza, mpaka akimpata, alale naye. Kisha Amunoni akaingiwa na machukizo makubwa sana ya kuchukizwa naye, nayo hayo machukizo yake ya kuchukizwa naye yakawa makubwa kuliko ule upendo wake wa kwanza wa kumpenda; kwa hiyo Amunoni akamwambia: Ondoka, uende zako! Naye akamwambia: La, sivyo! Kibaya hiki cha kunifukuza kingekuwa kikubwa kuliko kile, ulichonifanyizia, lakini akakataa kumsikia, akamwita kijana aliyemtumikia, akamwambia: Mtoeni huyu humu mwangu, aende nje! Tena funga mlango, akiisha kutoka. Naye alikuwa amevaa rinda refu la nguo za rangi, kwani ndiyo mavazi, watoto wa kike wa mfalme waliyoyavaa siku za kuwa wanawali. Yule mtumishi wake alipomtoa nje na kufunga mlango, alipokwisha kutoka, Tamari akachukua uvumbi, akautia kichwani pake, akalirarua lile rinda la nguo za rangi, alilokuwa amelivaa, akabandika mkono kichwani pake, akaenda zake na kulia. Ndipo, Abisalomu alipomwuliza umbu lake: Umbu lako Amunoni amekuwa kwako? Umbu langu, sasa nyamaza tu! Ndiye umbu lako. Neno hili usiliweke moyoni mwako! Basi, Tamari akakaa na ukiwa wake nyumbani mwa Abisalomu, umbu lake. Mfalme Dawidi alipoyasikia mambo haya, akachafuka sana. Lakini Abisalomu hakusema na Amunoni wala neno baya wala jema, kwani Abisalomu alimchukia Amunoni, kwa kuwa alimchukua umbu lake Tamari kwa nguvu. Miaka miwili ilipopita, Abisalomu akajipatia watu wa kukata manyoya ya kondoo kule Baali-Hasori upande wa Efuraimu; ndipo, Abisalomu alipowaalika wana wote wa mfalme. Abisalomu akaja hata kwa mfalme, akamwambia: Tazama, wako wenye kukata manyoya ya kondoo kwa mtumishi wako, mfalme naye na aje pamoja na watumishi wake kwa mtumishi wako! Mfalme akamwambia Abisalomu: Sivyo, mwanangu, tusije sote kwako, tusikulemee. Hata alipomhimiza, hakutaka kwenda, ila akambariki. Abisalomu akamwambia: Kama huji, ndugu yangu Amunoni na aende na sisi. Mfalme akamwuliza: Unamtakia nini kwenda na wewe? Abisalomu alipomhimiza, akampa Amunoni ruhusa kwenda pamoja naye pamoja na wana wote wa mfalme. Kisha Abisalomu akawaagiza vijana wake kwamba: Angalieni! Moyo wa Amunoni utakapochangamka kwa kunywa mvinyo, nitawaambieni: Mpigeni Amunoni! Ndipo, mtakapomwua pasipo kuogopa. Kwani ni mimi ninayewaagiza ninyi kuvifanya. Jipeni mioyo, mpate kuwa wenye nguvu! Vijana wa Abisalomu wakamfanyizia Amunoni, kama Abisalomu alivyowaagiza. Ndipo, wana wote wa mfalme walipoondoka, wakapanda kila mmoja nyumbu wake, wakakimbia. Hao walipokuwa njiani, Dawidi akapata habari kwamba: Abisalomu amewaua wana wote wa mfalme, asisalie kwao hata mmoja. Ndipo, mfalme alipoinuka, akayararua mavazi yake, akajilaza chini, nao watumishi wake wote wakawa wamesimama wenye mavazi yaliyoraruliwa. Naye Yonadabu, mwana wa Simea, kaka yake Dawidi, akaanza kusema kwamba: Bwana wangu asiwaze, ya kwamba wamewaua vijana wote walio wana wa mfalme, kwani Amunoni amekufa peke yake, kwani shauri hili lilikuwa limekatwa na kinywa chake Abisalomu tangu siku ile, yule alipomchukua umbu lake Tamari kwa nguvu. Sasa bwana wangu mfalme asiliweke neno hili moyoni mwake la kwamba: Wana wote wa mfalme wamekufa! Ila ni Amunoni peke yake aliyekufa. Lakini Abisalomu alikuwa amekimbia. Kijana wa mfalme aliyekuwa mlinzi alipoyainua macho yake, aone vema, mara akaona watu wengi wanaotelemka katika njia iliyoko mgongoni kwake upande wa milimani. Ndipo, Yonadabu alipomwambia mfalme: Tazama, wana wa mfalme wanakuja! Kama mtumishi wako alivyosema, ndivyo, inavyokuwa. Alipokwisha kusema, ndipo, wana wa mfalme walipofika, wakapaza sauti zao, wakalia; naye mfalme na watumishi wake wote wakalia kilio kikubwa sana. Abisalomu alipokimbia akaenda kwa Talmai, mwana wa Amihudi, mfalme wa Gesuri. Naye Dawidi akamlilia mwanawe kila siku. Naye Abisalomu akakaa miaka mitatu kule Gesuri, alikokwenda kwa kukukimbilia. Naye mfalme Dawidi akatamani sana kwenda kumtokea Abisalomu, alipokwisha kuutuliza moyo wake kwa ajili ya kufa kwake Amunoni. Yoabu, mwana wa Seruya, alipotambua, ya kuwa moyo wa mfalme umerudi kumwelekea Abisalomu, Yoabu akatuma Tekoa kumchukua huko mwanamke aliye mwerevu wa kweli, akamwambia: Jitendekeze kuwa mwenye kufiwa, ukivaa nguo za matanga pasipo kujipaka mafuta, uwe sawasawa na mwanamke anayemlilia mfu siku nyingi. Kisha uende kwa mfalme, mwambie maneno kama haya! Naye Yoabu akamwambia, atakayoyasema na kinywa chake. Basi, huyo mwanamke wa Tekoa akaja kusema na mfalme akijiangusha chini kifudifudi, kwamba amwangukie, akasema: Nisaidie, mfalme! Mfalme alipomwuliza: Una nini? akasema: Mimi ni mwanamke mjane kweli, maana mume wangu amekufa. Tena kijakazi wako alikuwa na wana wawili wa kiume, nao wakagombana shambani; kwa kuwa hakuwako aliyewaamua, mmoja akampiga ndugu yake, mpaka akamwua. Mara ukoo wote ukamwinukia kijakazi wako na kusema: Mtoe aliyempiga ndugu yake, tumwue kwa ajili ya roho ya ndugu yake, aliyemwua, tumtoweshe naye atakayelichukua fungu lake! Ndivyo, wanavyotaka kulizima nalo kaa la mwisho lililosalia, wasimwachie mume wangu huku nchini jina wala sao lo lote. Mfalme akamwambia huyu mwanamke: Jiendee nyumbani kwako! Mimi nitatoa amri kwa ajili yako. Ndipo, huyu mwanamke wa Tekoa alipomwambia mfalme: Bwana wangu mfalme, manza ni zangu na za mlango wa baba yangu, mfalme hayumo, wala kiti chake cha kifalme. Mfalme akamwambia: Atakayekutakia kitu mlete kwangu, asiendelee kukugusa tena. Akajibu: Mfalme, mkumbuke Bwana Mungu wako, mwenye kulipiza damu asizidi kufanya mabaya, wakimwangamiza mwanangu. Akasema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, unywele mmoja tu wa mwanao hautaanguka chini. Ndipo, huyu mwanamke alipomwuliza: Kumbe kijakazi wako ataweza kumwambia bwana wangu mfalme neno? Akajibu: Sema Basi! huyu mwanamke akasema: Mbona unawawazia watu walio wa Mungu mambo kama hayo? Kwa kulisema neno hili mfalme anakuwa kama mtu aliyekora manza, mfalme asipomrudisha yule mtu wake aliyefukuzwa. Kwani hatuna budi kufa; tunafanana na maji yaliyomwagika chini, yasiyowezekana kukusanywa tena; lakini Mungu haondoi roho ya mtu, ila huwaza, jinsi inavyowezekana, mtu aliyefukuzwa asikae na kufukuzwa kwake vivyo hivyo. Sasa nimefika kumwambia bwana wangu mfalme neno hili, kwa kuwa watu wamenitisha. Kwa hiyo kijakazi wako alisema: Na nimwambie mfalme, labda mfalme atalifanya neno la kijakazi wake. Kwani mfalme, atanisikia, amponye kijakazi wake mkononi mwa yule mtu anayetaka kuniangamiza pamoja na mwanangu, nisikae na fungu, Mungu alilonipa. Kwa hiyo kijakazi wako akasema: Neno la bwana wangu mfalme litanipatia utulivu, kwani kama malaika wa Mungu alivyo, ndivyo, bwana wangu mfalme alivyo, asikie mema na mabaya. Naye Bwana Mungu wako awe na wewe! Mfalme akajibu na kumwambia huyu mwanamke: Usinifiche kabisa, nitakalokuuliza! Huyu mwanamke akasema: Bwana wangu mfalme na aseme! Ndipo, mfalme alipouliza: Je? Mkono wa Yoabu haumo katika mambo haya yote? Huyu mwanamke akajibu kwamba: Hivyo roho yako, bwana wangu mfalme, ilivyo nzima, hakuna njia kuumeni wala kushotoni ya kupita penye maneno yote, bwana wangu mfalme aliyoyasema; kweli mtumishi wako Yoabu ndiye aliyeniagiza hivyo, naye ndiye aliyeniambia na kinywa chake, kijakazi wako atakayoyasema. Kwa kutaka kuligeuza jambo hili, upande wake mwingine uonekane, mtumishi wako Yoabu amelifanya hili neno, naye bwana wangu anao werevu wa kweli ulio kama werevu wa malaika wa Mungu wa kuyajua yote yaliyopo nchini. Kisha mfalme akamwambia Yoabu: Tazama, nitalifanya jambo hili. Nenda, umrudishe yule kijana Abisalomu. Ndipo, Yoabu alipojiangusha chini kifudifudi kumwangukia na kumbariki mfalme, kisha Yoabu akasema: Leo hivi mtumishi wako anajua, ya kuwa nimeona upendeleo machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amelifanya neno la mtumishi wake. Kisha Yoabu akaondoka, akaenda Gesuri, akamleta Abisalomu humo Yerusalemu. Lakini mfalme akasema: Na aende kuingia nyumbani mwake pasipo kuonana na mimi uso kwa uso. Kwa hiyo Abisalomu akaingia nyumbani mwake pasipo kuonana na mfalme uso kwa uso. Kwao Waisiraeli wote hakuwako mtu, watu waliyemsifu sana kwa uzuri wake wa mwili kama Abisalomu, toka wayo wa mguu wake mpaka kwenye utosi wake hakikuwako cho chote kisicho kizuri. Kila mara siku za mwaka mmoja zilipopita akazinyoa nywele za kichwani, naye huzinyoa, zikimlemea kwa uzito; tena alipokwisha kuzinyoa huzipima hizo nywele za kichwani pake, nazo huwa kama sekeli 200, ndio ratli 7 kwa kipimo cha mfalme. Kisha kwake Abisalomu wakazaliwa wana wa kiume watatu na wa kike mmoja, jina lake Tamari; naye alikuwa mwanamke mwenye sura nzuri. Abisalomu alipokaa Yerusalemu miaka miwili pasipo kuonana na mfalme uso kwa uso, ndipo, Abisalomu alipotuma kwa Yoabu, apate kumtuma kwa mfalme, lakini akakataa kufika kwake. Akatuma tena mara ya pili, lakini akakataa kufika. Ndipo, alipowaambia watumishi wake: Tazameni, liko shamba la Yoabu linalopakana na langu, nalo ni la mawele yake. Nendeni, mlichome moto! Ndipo, watumishi wa Abisalomu walipolichoma moto hilo shamba. Ndipo, Yoabu alipoondoka, akaja kwa Abisalomu nyumbani kwake, akamwuliza: Mbona watumishi wako wamelichoma shamba langu moto? Abisalomu akamjibu Yoabu: Tazama, nalituma kwako kwamba: Njoo hapa, nikutume kwa mfalme kumwambia: Mbona nimekuja na kutoka Gesuri? Ingenifaa, nikae huko bado. Lakini sasa na nitokee usoni pake mfalme, kama ziko manza, nilizozikora, basi, na aniue. Yoabu alipokwenda kwa mfalme kumpasha hizi habari, akamwita Abisalomu; naye alipofika kwa mfalme akamwangukia mfalme na kujiangusha chini kifudifudi, ndipo, mfalme alipomnonea Abisalomu. Hayo yalipokwisha, Abisalomu akajipatia magari na farasi na watu 50, wamtangulie na kupiga mbio. Kila siku Abisalomu hujidamka, kisha husimama mjini kando kwenye lango la mji. Basi, kila mtu aliyepita mwenye shauri la kwenda kwa mfalme kuamuliwa, Abisalomu humwita kwake na kumwuliza: Wewe unatoka mji gani? Aliposema: Mtumishi wako ni mmoja wao wa mashina ya Waisiraeli, Abisalomu humwambia: Tazama, shauri lako ni zuri, linapasa, lakini kwa mfalme hakuna atakayekusikiliza. Kisha Abisalomu husema: Kama wangeniweka mimi kuwa mwamuzi katika nchi hii, ningeyakata vema mashauri ya kila mtu atakayekuja kwangu mwenye neno la kugombana na mwenye shauri lo lote. Napo, mtu alipomkaribia, amwangukie, hukunjua upesi mkono wake, apate kumnonea. Hivyo ndivyo, Abisalomu alivyowafanyizia Waisiraeli wote waliokwenda shaurini kwa mfalme, navyo ndivyo, alivyoiiba mioyo ya waume wa Waisiraeli. Miaka 40 ilipokwisha, Abisalomu akamwambia mfalme: Na niende kumlipa Bwana huko Heburoni, niliyomwapia ya kumtolea. Kwani mtumishi wako ameapa kiapo, nilipokaa Gesuri kwa Washami, cha kwamba: Kama Bwana atanirudisha Yerusalemu, nitamtumikia Bwana. Mfalme akamwambia: Nenda na kutengemana! Basi, akaondoka, akaenda Heburoni. Kisha Abisalomu akatuma wapelelezi kwa mashina yote ya Waisiraeli kwamba: Mtakaposikia, mabaragumu yakilia, semeni: Abisalomu amepata ufalme Heburoni! Pamoja na Abisalomu walikwenda toka Yerusalemu watu 200 walioalikwa naye, waliokwenda pasipo mawazo mabaya yo yote, maana hawakujua neno lo lote. Abisalomu akatuma kumchukua Ahitofeli wa Gilo aliyekuwa mmoja wao waliomwongoza Dawidi mashaurini; akamtoa huko Gilo mjini kwake, alipochinja ng'ombe za tambiko. Hivyo lile fujo likapata nguvu, nao watu waliorudi upande wa Abisalomu wakaendelea kuwa wengi zaidi. Mtu alipofika kwa Dawidi na kumpasha habari ya kwamba: Mioyo ya waume wa Waisiraeli imegeuka kumfuata Abisalomu, Dawidi akawaambia watumishi wake wote, aliokuwa nao Yerusalemu: Haya! Ondokeni, tukimbie! Kwani hatutapata kupona, Abisalomu akitujia. Pigeni mbio, twende, asitukamate upesi na kutufanyizia mabaya, akiwaua waliomo humu mjini kwa ukali wa panga. Watumishi wa mfalme wakamwambia mfalme: Yote yampendezayo bwana wetu mfalme, basi, sisi watumishi wako tuko. Kisha mfalme akatoka pamoja nao wote waliokuwamo nyumbani mwake, wakienda kwa miguu yao; mfalme akaacha masuria kumi tu wa kuiangalia nyumba. Mfalme alipokwisha kutoka hivyo pamoja na watu wake wote, wakienda kwa miguu, wakasimama penye nyumba ya mwisho. Ndipo, watumishi wake wote walipopita kando yake, nao Wakreti wote na Wapuleti wote na Wagati wote, watu 600 waliotoka Gati wakienda kwa miguu, wote pia wakapita hapo mbele ya mfalme. Mfalme akamwuliza Itai wa Gati: Mbona wewe nawe utakwenda pamoja na sisi? Rudi, ukae kwa mfalme! Kwani wewe u mgeni aliyefukuzwa kwao; haya! Nenda zako! Umefika jana; basi, leo nitawezaje kukusumbua na kukuchukua kwenda na sisi? Mimi ninakwenda na kutangatanga po pote, nitakapokwenda, lakini wewe rudi! Nao ndugu zako warudishe pamoja na wewe, nao upole na welekevu na uwakalie! Itai akamjibu mfalme akisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena bwana wangu mfalme alivyo mzima, mahali, bwana wangu mfalme atakapokuwa, kama ni pa kufia, au kama ni pa kuponea, ndipo, mtumishi wako naye atakapokuwa. Ndipo, Dawidi alipomwambia Itai: Basi, nenda nawe, upite! Naye Itai wa Gati akapita na watu wake wote na wake na watoto wote waliokuwa naye. Watu wote wa nchi hiyo wakalia na kuzipaza sauti zao pamoja na watu wote walipita hapo, mfalme alipouvuka mto wa Kidoroni pamoja na wale watu wote waliopita mbele yake, wakajielekeza kushika njia ya kwenda nyikani. Mara akaja naye Sadoki pamoja na Walawi wote waliolichukua Sanduku la Agano la Mungu; wakalitua Sanduku la Agano, naye Abiatari akatambika, mpaka watu wote walipokwisha kupita na kutoka mjini. Mfalme akamwambia Sadoki: Lirudishe mjini Sanduku la Mungu! Kama nitaona upendeleo machoni pa Bwana, atanirudisha, nipate kuliona tena napo mahali, linapokaa. Lakini kama ataniambia hivi: Sipendezwi na wewe, basi, niko, anifanyizie atakayoyaona kuwa mema. Kisha mfalme akamwambia mtambikaji Sadoki: Je? Wewe siwe mtazamaji? Rudi mjini na kutengemana pamoja na mwanao Ahimasi na Yonatani, mwana wa Abiatari, hawa wana wenu wawili waende nanyi. Tazameni, mimi nitakawilia penye mbuga za nyikani, mpaka itafika kwangu habari toka kwenu. Kwa hiyo Sadoki na Abiatari wakalirudisha Sanduku la Mungu Yerusalemu, wakakaa huko. Dawidi akapapanda pa kuukwelea mlima wa michekele, akaenda akilia, nacho kichwa chake kilikuwa kimefunikwa, naye mwenyewe alikwenda pasipo kuvaa viatu; hata watu wote waliokuwa naye walikuwa wamekifunika kila mtu kichwa chake, nao wakawa wakipanda na kulia. Walipompasha Dawidi habari ya kwamba: Ahitofeli yuko kwa Abisalomu pamoja nao waliovunja maagano, Dawidi akasema: Bwana na aligeuze shauri la Ahitofeli kuwa ujinga! Dawidi alipofika pale juu, watu wanapomtambikia Mungu, mara akaja Mwarki Husai akimwendea njiani mwenye kanzu iliyoraruliwa na mwenye mchanga kichwani pake. Dawidi akamwambia: Ukienda pamoja nami safari yangu, ndipo, utakaponilemea. Lakini ukirudi mjini na kumwambia Abisalomu: Mimi nitakuwa mtumishi wako, mfalme; kama nilivyokuwa mtumishi wa baba yako tangu kale, ndivyo, nitakavyokuwa sasa mtumishi wako. Basi, ndivyo, utakavyolitengua shauri la Ahitofeli. Je? Mle mjini hunao wale watambikaji Sadoki na Abiatari? Iwe hivyo: kila neno, utakalolisikia nyumbani mwa mfalme, uwasimulie wale watambikaji Sadoki na Abiatari. Tazama, wanao mle mjini wana wao wawili: Sadoki anaye Ahimasi, Abiatari anaye Yonatani. Kwa kuwatumia hao mtaweza kuniletea kila neno, mtakalolisikia. Ndipo, Husai aliyekuwa rafiki yake Dawidi aliporudi mjini, Abisalomu alipoingia Yerusalemu. Dawidi alipokwisha kupita kidogo hapo kilimani juu, mara Siba, kijana wa Mefiboseti, akamwendea njiani, anao punda wawili waliotandikwa kuchukua mikate 200 na maandazi 100 ya zabibu na maandazi 100 ya kuyu na kiriba cha mvinyo. Mfalme alipomwuliza: Haya unanileteaje? Siba akasema: Punda ni wa kuchukua walio wa mlango wa mfalme, nayo mikate na maandazi ni ya kula ya vijana, nayo mvinyo ni ya kunywa, mtu akichoka nyikani. Mfalme akamwuliza: Naye mwana wa bwana wako yuko wapi? Ndipo, Siba alipomwambia mfalme: Tazama, anakaa Yerusalemu, kwani amesema: Leo wao wa mlango wa Isiraeli watanirudishia ufalme wa baba yangu. Ndipo, mfalme alipomwambia Siba: Tazama, mali zote za Mefiboseti ni zako! Siba naye akasema: Ninakuangukia, nione tena upendeleo machoni pako, bwana wangu mfalme! Mfalme Dawidi alipofika Bahurimu, mara mle akatoka mtu wa ukoo wao walio mlango wa Sauli, jina lake Simei, mwana wa Gera; alipotoka alikwenda akitukana. Tena akamtupia Dawidi mawe nao watumishi wote wa mfalme Dawidi, nao watu wote na mafundi wa vita wote walikuwa kuumeni na kushotoni kwake. Hivi ndivyo, Simei alivyosema akitukana: Toka! Toka, wewe mtu wa damu, wewe mtu usiyefaa! Bwana anakulipisha damu zao wote walio wa mlango wa Sauli, ambaye umejifanya kuwa mfalme mahali pake. Yeye Bwana ameutia ufalme mkononi mwa mwanao Abisalomu, wewe nawe umepatwa na mabaya, kwa kuwa wewe u mtu wa damu. Ndipo, Abisai, mwana wa Seruya, alipomwambia mfalme: Mbona mbwa mfu huyu anamtukana bwana wangu mfalme? Acha, nimwendee, nimkate kichwa mara moja! Lakini mfalme akasema: Tuna bia gani mimi nanyi, wana wa Seruya? Na atukane hivyo; kama Bwana amemwagiza: Mtukane Dawidi! yuko nani awezaye kusema: Mbona unafanya hivyo? Kisha Dawidi akamwambia Abisai na watumishi wake wote: Tazameni, mwanangu aliyetoka kiunoni mwangu anaitaka roho yangu! Sasa huyu mtu wa Benyamini anafanya nini? Mwacheni, atukane, kwani Bwana amemwagiza hivyo. Labda Bwana atautazama ukiwa wangu, yeye Bwana anirudishie mema kwa hivyo, huyu anavyonitukana leo hivi. Kisha Dawidi akaenda zake na watu wake, Simei naye akaenda kandokando ya mlima karibu yake akiendelea kutukana na kumtupia mawe na kumpiga kokotokokoto. Mfalme na watu wote waliokuwa naye walipofika mahali fulani walikuwa wamechoka, wakapumzika hapo. Abisalomu na Waisiraeli wote walipoingia Yerusalemu, Ahitofeli alikuwa naye. Ikawa, Mwarki Husai, yule rafiki yake Dawidi, alipofika kwa Abisalomu, Husai akamwambia Abisalomu: Pongezi, mfalme! Pongezi, mfalme! Abisalomu akamwuliza Husai: Huu ndio welekevu, unaomfanyizia rafiki yako? Mbona hukuenda pamoja na rafiki yako? Husai akamwambia Abisalomu: Sivyo! Ila yule, Bwana aliyemchagua na watu hawa wote na waume wote wa Waisiraeli, basi, nami ni mtu wake, nikae naye! Tena nimtumikie nani? Siye mwanawe? Kama nilivyomtumikia baba yako, ndivyo, nitavyokutumikia. Abisalomu akamwambia Ahitofeli: Haya! Nipeni shauri, jinsi tutakavyofanya! Ahitofeli akamwambia Abisalomu: Ingia kwao masuria wa baba yako, aliowaacha kuiangalia nyumba! Hapo, Waisiraeli wote watakaposikia, ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako, ndipo, mikono yao wote waliorudi upande wako itakapopata nguvu. Kisha wakampigia Abisalomu hema darini, naye Abisalomu akaingia kwao masuria wa baba yake machoni pao Waisiraeli wote. Siku zile shauri, alilolitoa Ahitofeli likawa sawa na neno, mtu aliloliuliza kwake Mungu. Ndivyo, mashauri yote ya Ahitofeli, yalivyowaziwa kuwa, kama siku za Dawidi, vivyo hivyo hata siku za Abisalomu. Ahitofeli akamwambia Abisalomu: Na nichague watu 12000, niondoke kumfuata Dawidi upesi na usiku. Nitakapofika kwake, atakuwa amechoka, nayo mikono yake itakuwa imelegea; nikimstusha, akiwa hivyo, watu wote waliokuwa naye wakatimbia, nami nitampata mfalme, nimpige, akiwa peke yake. Kisha nitawarudisha watu wote kwako; hao watu wote, unaowatafuta wewe, watakaporudi, basi, huu ukoo wote mzima utakaa na kutengemana. Neno hili likanyoka machoni pake Abisalomu napo machoni pao wazee wote wa Waisiraeli. Lakini Abisalomu akasema: Mwite naye Mwarki Husai, tuyasikie nayo yaliyomo kinywani mwake! Husai alipofika kwake Abisalomu, Abisalomu akamwambia kwamba: Ahitofeli amesema haya na haya; nasi tulifanye, alilolisema, au tuache? Sema wewe! Husai akamwambia Abisalomu: Mara hii shauri, Ahitofeli alilolitoa, si jema. Husai akasema: Wewe unamjua baba yako na watu wake, ya kuwa wao ndio mafundi wa vita wenye ukali rohoni mwao kama chui mke aliyenyang'anywa watoto wake, naye baba yako ni mtu wa vita, hatalala usiku kwa watu wake. Tazama, sasa yeye amekwisha kujificha katika shimo moja au penginepo palipo hivyo; lakini itakapokuwa, mwanzoni watu wa kwetu wauawe kwa kupigana nao, kila atakayevisikia atasema: Watu wanaomfuata Abisalomu wameshindwa katika mapigano. Ndipo, hata mwenye nguvu aliye mwenye moyo kama wa simba atakapoyeyuka kabisa, kwani Waisiraeli wote wanajua, ya kuwa baba yako ni fundi wa vita, nao watu waliokuwa naye ni wenye nguvu. Kwa hiyo shauri langu ni hili: Kwako na wakusanyike Waisiraeli wote toka Dani mpaka Beri-Seba, wawe wengi kama mchanga ulioko ufukoni kwenye bahari, kisha mwenyewe nenda nao vitani! Kisha tutamshambulia mahali pamoja; atakapoonekana, tumwangukie, kama umande unavyoiangukia nchi, tusisaze kwake hata mtu mmoja miongoni mwao wote waliokuwa naye! Kama atakimbilia mjini, Waisiraeli wote na waupeleke mji huo kamba, tuufunge, tuuvute na kuukokota mpaka mtoni, pasionekane pake tena hata kijiwe kimoja tu. Ndipo, Abisalomu na watu wote wa Waisiraeli waliposema: Shauri la Mwarki Husai ni jema kuliko shauri la Ahitofeli. Lakini alikuwa Bwana aliyeagiza kulitengua shauri jema la Ahitofeli, kusudi Bwana ampatie Abisalomu mabaya. Kisha Husai akawaambia watambikaji Sadoki na Abiatari: Ahitofeli amempa Abisalomu na wazee wa Waisiraeli mashauri haya na haya, lakini mimi nimewapa shauri hili. Sasa tumeni upesi kumpasha Dawidi habari za kwamba: Usilale usiku huu penye mbuga za nyikani, sharti uvuke mtoni, mfalme asimezwe na mabaya pamoja na watu wote waliokuwa naye. Yonatani na Ahimasi walikuwa wakikaa penye Chemchemi ya Wafua nguo; kwa hiyo kijakazi mmoja akaenda kuwapasha habari, nao wakaenda kumpasha mfalme Dawidi hizo habari. Ilikuwa hivyo, watu wasipate kuwaona wakiingia mjini. Lakini kijana aliwaona, naye akampasha Abisalomu habari. Nao wote wawili wakaenda na kupiga mbio, wakaingia nyumbani mwa mtu mle Bahurimu, naye alikuwa na kisima uani pake; ndimo, walimoshukia. Kisha mwanamke akachukua blanketi, akalitanda juu ya kisima hicho, akaanika humo ngano zilizotwangwa, lisijulikane neno lo lote. Watumishi wa Abisalomu walipofika nyumbani kwa huyu mwanamke na kumwuliza: Ahimasi na Yonatani wako wapi? huyu mwanamke akwaambia: Wamekwenda kukivuka kile kijito. Basi, walipowatafuta pasipo kuwaona, wakarudi Yerusalemu. Hao walipokwisha kwenda, wale wakatoka kisimani, wakaenda kumpasha mfalme Dawidi habari, wakamwambia Dawidi: Ondokeni, mvuke upesi mtoni! Kwani haya ndiyo mashauri, Ahitofeli aliyoyatoa kwa ajili yenu. Ndipo, Dawidi alipoondoka pamoja na watu wote waliokuwa naye, wakauvuka Yordani. Mapema yalipopambazuka, hakusalia hata mmoja asiyeuvuka Yordani. Ahitofeli alipoona, ya kuwa shauri lake halikufanywa, akamtandika punda wake, akaondoka kwenda nyumbani mjini kwake, akayatengeneza mambo ya nyumbani, kisha akajinyonga, akafa, akazikwa kaburini mwa baba yake. Dawidi alipofika Mahanaimu, ndipo, Abisalomu alipouvuka Yordani, yeye na watu wote wa Waisiraeli pamoja naye. Naye Abisalomu alimweka Amasa kuwa mkuu wa vikosi mahali pake Yoabu; Amasa alikuwa mwana wa mtu aitwaye Itira wa Isiraeli; ndiye aliyeingia kale kwa Abigaili, binti Nahasi, umbu la Seruya aliyekuwa mama yake Yoabu. Waisiraeli na Abisalomu wakapiga makambi katika nchi ya Gileadi. Ikawa, Dawidi alipoingia Mahanaimu, ndipo, Sobi, mwana wa Nahasi wa Raba wa wana wa Amoni, na Makiri, mwana wa Amieli wa Lo-Debari, na Mgileadi Barzilai wa Roglimu, walipoleta vitanda na mabakuli na vyombo vya udongo na ngano na mawele na unga na bisi na kunde na mbaazi na bisi za mchele, na asali na siagi na mbuzi na kondoo na maziwa mabivu ya ng'ombe, wakampelekea Dawidi na watu waliokuwa naye, wayale, kwani walisema: Watu hawa wana njaa, tena wamechoka kwa kupatwa na kiu za nyikani. Dawidi akawakagua watu waliokuwa naye, akawawekea wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia. Kisha Dawidi akawatuma hao watu kwenda vitani, akawatia fungu la tatu mkononi mwa Yoabu, fungu jingine la tatu mkononi mwa Abisai, mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, tena fungu jingine la tatu mkononi mwa Itai wa Gati. Kisha mfalme akawaambia hao watu: Hata mimi nitatoka pamoja nanyi kwenda vitani. Lakini watu wakasema: Usitoke pamoja nasi! Kwani kama itakuwa, tukimbie, wale hawatatuelekezea sisi mioyo; ijapo watu wa kwetu wafe kama nusu nzima, hawatuelekezea sisi mioyo, kwani wewe u kama watu elfu kumi wa kwetu. Kwa hiyo itatufaa sasa, ukae mjini, upate kuja kutusaidia. Mfalme akawaitikia kwamba: Yaliyo mema machoni penu, basi, nitayafanya. Kisha mfalme akaja kusimama kando penye lango la mji, nao watu wote wakatoka mia kwa mia, na elfu kwa elfu. Ndipo, mfalme alipomwagiza Yoabu na Abisai na Itai wa Gati kwamba: Nataka hili tu, mmwendee mvulana Abisalomu kwa upole! watu wote wakayasikia, mfalme alipowaagiza wakuu wote hayo kwa ajili ya Abisalomu. Kisha watu wakawaendea Waisiraeli maporini, nayo mapigano yakawa katika mwitu wa Efuraimu. Nao watu wa Waisiraeli wakapigwa kabisa na watumishi wa Dawidi, wapata hata 20000, nayo mapigano yalikuwa yameenea po pote katika nchi hiyo, nao watu, mwitu uliowala, walikuwa wengi kuliko wao, panga ziliowala siku hiyo. Ikatukia, watumishi wa Dawidi wamwone Abisalomu, naye Abisalomu alikuwa amepanda nyumbu; huyo nyumbu alipopita chini ya mkwaju mkubwa wenye matawi mengi yaliyofungamana, mara tawi moja likakikamata kichwa chake mlemle katika mkwaju, hivyo akaangikwa katikati ya mbingu na nchi, kwani nyumbu aliyekuwa chini yake alikimbia. Mtu mmoja aliyeviona akampasha Yoabu habari akisema: Tazama, nimemwona Abisalomu, alivyoangikwa mkwajuni. Ndipo, Yoabu alipomwambia yule mtu aliyempasha habari hiyo: Kama umemwona hivyo, sababu gani kukumpiga, aanguke chini, nami nikakupa fedha kumi na mkanda mmoja? Yule mtu akamwambia Yoabu: Ijapo ningepimiwa mimi fedha elfu mikononi mwangu, nisingemkunjulia mwana wa mfalme mkono wa kumpiga, kwani masikioni petu mfalme amekuagiza wewe na Abisai na Itai kwamba: Niangalieni mvulana Abisalomu! Kwani ningaliipotoa roho yake, jambo hilo lote halingalifichikana kwa mfalme, nawe wewe ungaliniinukia. Yoabu akasema: Haifai, nikijikawilisha huku kwako. Akachukua mikuki mitatu mkononi mwake, akamchoma nayo Abisalomu moyoni, angaliko mzima mlemle mkwajuni. Kisha vijana kumi waliomchukulia Yoabu mata wakamzunguka Abisalomu, wakamaliza kumwua kwa kumpiga. Kisha Yoabu akapiga baragumu; ndipo, watu waliporudi wakiacha kuwakimbiza Waisiraeli, kwani ndivyo, Yoabu alivyowazuia watu wake. Wakamchukua Abisalomu, wakamtupa mle mwituni katika shimo kubwa, juu yake wakakusanya mawe kuwa chungu kubwa sana. Kisha Waisiraeli wote wakakimbilia kila mtu hemani kwake. Naye Abisalomu alipokuwa mzima bado alichukua nguzo ya mawe kule Bondeni kwa Mfalme, akaisimamisha, kwani alisema: Mimi sina mwana wa kulikumbusha jina langu; kwa hiyo aliiita ile nguzo ya mawe kwa jina lake, ikaitwa Mkono wa Abisalomu hata siku hii ya leo. Ahimasi, mwana wa Sadoki, akasema: Na nipige mbio kumpelekea mfalme utume mwema, kwani Bwana amemwamulia na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Lakini Yoabu akamwambia: Siku hii ya leo wewe hu mtu wa kupeleka utume; siku nyingine utapeleka utume, lakini siku hii ya leo hutapeleka utume wewe, kwa kuwa mwana wa mfalme amekufa. Kisha Yoabu akamwambia Mnubi: Nenda kumpasha mfalme habari za mambo, uliyoyaona! Yule Mnubi akamwangukia Yoabu, kisha akaenda na kupiga mbio. Lakini Ahimasi, mwana wa sadoki, akamwambia Yoabu tena: Nami na niende mbiombio, nimfuate yule Mnubi. Yoabu akamwambia: Wewe utakimbilia nini, mwanangu? kwani hakuna ujira, utakaopewa. Akajibu: Haidhuru, nitakwenda nami na kupiga mbio. Akamwambia: Haya!, Ndipo, Ahimasi alipopiga mbio na kushika njia ya nchi ya tambarare; ndivyo, alivyompita yule Mnubi. Naye Dawidi alikuwa amekaa katikati ya malango mawili; mlinzi alipopanda humo langoni kufika juu yake ukutani na kuyainua macho yake, achungulie, mara akaona mtu anayekimbia peke yake. Ndipo, mlinzi alipoita, akampasha mfalme habari hizo; naye mfalme akasema: Kama yuko peke yake, basi, kinywani mwake umo utume mwema. Huyu alipofika karibu, mlinzi akaona mtu mwingine anayekimbia peke yake; ndipo, mlinzi alipomwita mlinda lango, akamwambia: Tazama, yuko mtu anayekimbia peke yake! Mfalme akasema: Huyu naye analeta utume mwema. Kisha mlinzi akasema: Mbio zake yule wa kwanza ninaziona kuwa kama mbio za Ahimasi, mwana wa Sadoki. Mfalme akasema: Ni mtu mwema huyu, naye anakuja kuleta utume mwema. Ahimasi akaita na kumwambia mfalme: Pongezi! Kisha akamwangukia mfalme na kujiangusha chini kifudifudi, akasema: Bwana Mungu wako na atukuzwe! Kwani wao waliomwinulia bwana wangu mfalme mikono yao amewatoa. Mfalme akauliza: Mvulana Abisalomu hajambo? Ahimasi akasema: Nimeona mtutumo mkubwa, mtumishi wa mfalme Yoabu alipomtuma mtumishi wako, lakini sikujua, kama kuna nini. Mfalme akamwambia: Zunguka, uje kusimama hapa! Naye akazunguka, akasimama hapo. Mara yule Mnubi akaja, naye akasema kwamba: Bwana wangu mfalme na ausikie huu utume mwema, ya kuwa Bwana amekuamulia leo na kukuokoa mikononi mwao wote waliokuinukia. Mfalme akamwuliza huyu Mnubi naye: Mvulana Abisalomu hajambo? Huyu Mnubi akasema: Adui wote wa mfalme na wafanyiziwe kama huyo mvulana! Nao wote waliokuinukia kufanya mabaya na wawe hivyo! Ndipo, mfalme alipostuka, akapanda katika chumba cha juu hapo langoni, akalia akisema hivyo, akajiendea na kusema hivyo: Mwanangu Abisalomu! Mwanangu! Mwanangu Abisalomu! Ningalikufa mimi mahali pako! Mwanangu Abisalomu! Mwanangu! Yoabu alipopashwa habari kwamba: Tazama, mfalme analia na kumwombolezea Abisalomu, ndipo, wokovu wa siku hiyo ulipowageukia watu wote kuwa uchungu, kwani watu walisikia siku hiyo kwamba: Mfalme anamsikitikia mwanawe. Kwa hiyo wakaingia mjini siku hiyo na kujifichaficha kama wezi, wakawa kama watu wanaotoka vitani na kujifichaficha kama wezi, kwa kuwa wametoroka vitani. Mfalme akaufunika uso wake, naye mfalme akalia na kupaza sauti sana kwa kwamba: Mwanangu Abisalomu! Abisalomu mwanangu! Mwanangu! Ndipo, Yoabu alipoingia nyumbani mwa mfalme, akasema: Leo umezitia soni nyuso za watumishi wako wote, nao wameiponya leo roho yako nazo roho zao wanao wa kiume na wa kike nazo roho zao wake zako na masuria zako. Unawapenda wakuchukiao, ukawachukia wakupendao, kwani leo umevitokeza, ya kuwa wakuu na watumishi si kitu kwako, kwani leo nimevitambua hivi: kama Abisalomu angalikuwa mzima, kama sisi sote tungaliuawa, basi, hili jambo lingenyoka machoni pako. Lakini sasa inuka, utoke, useme na watumishi wako na kuituliza mioyo yao! Kwani ninaapa na kumtaja Bwana kwamba: Usipowatokea, hakuna mtu atakayelala kwako usiku huu, nayo mabaya yatakayokupata kwa ajili hii yatakuwa mabaya zaidi kuliko yote yaliyokupata tangu utoto wako mpaka sasa. Ndipo, mfalme alipoondoka, akaja kukaa langoni; nao watu walipowatangazia watu wote kwamba: Tazameni, mfalme amekaa langoni, watu wote wakaja kumtokea mfalme. Lakini Waisiraeli walikuwa wamekimbia kila mtu hemani kwake, Watu wote wakarudiana katika mashina yote ya Waisiraeli kwamba: Mfalme ametuponya mikononi mwa adui zetu, naye ndiye aliyetuponya mikononi mwa Wafilisti, naye hakuwa na budi kumkimbia Abisalomu na kutoka katika nchi hii. Naye Abisalomu, tuliyempaka mafuta, awe mfalme wetu, amekufa vitani; sasa mwakawiliaje tena kumrudisha mfalme? Kisha mfalme akatuma kwa watambikaji Sadoki na Abiatari kwamba: Waambieni wazee wa Waisiraeli kwamba: Mbona mwataka kuwa wa mwisho wa kumrudisha mfalme nyumbani mwake? Kwa maana lile shauri la Waisiraeli lilikuwa limefika nyumbani kwa mfalme. Ninyi m ndugu zangu, mifupa yetu ni ya mmoja, nazo nyama za miili yetu ni za mmoja; mbona mnataka kuwa wa mwisho wa kumrudisha mfalme? Naye Amasa mwambieni: Kumbe wewe na mimi mifupa yetu siyo ya mmoja, nazo nyama za miili yetu sizo za mmoja? Mungu na anifanyizie hivi na hivi, wewe usipopata kwangu kuwa mkuu wa vikosi siku zote mahali pake Yoabu! Ndivyo, alivyojipatia tena mioyo ya Wayuda wote kuwa ya mtu mmoja tu, nao wakatuma kwa mfalme kumwambia: Rudi wewe pamoja na watumishi wako wote! Ndipo, mfalme aliporudi; alipofika Yordani, Wayuda walikuwa wamefika Gilgali kumwendea mfalme njiani, wamvushe mfalme Yordani. Naye Mbenyamini Simei, mwana wa Gera, aliyekaa Bahurimu, akaja upesi, akashuka pamoja na watu wa Yuda kumwendea mfalme Dawidi njiani. Pamoja naye wakaja watu elfu toka nchi ya Benyamini, hata Siba, mtumishi wa nyumbani mwa Sauli, akaja na wanawe 15 na watumishi wake 20. Wao walikuwa wamevuka Yordani, mfalme alipokuwa hajaja bado. Mtumbwi wa kuwavusha walio wa nyumbani mwa mfalme ulipofika ng'ambo ya huko, mfalme aone, wanavyomfanyizia kazi nzuri, ndipo, Simei, mwana wa Gera, alipojiangusha chini machoni pa mfalme, alipotaka kuuvuka Yordani, akamwambia mfalme: Bwana wangu asiniwazie kuwa mwenye uovu, wala asiyakumbuke yale mapotovu, mtumwa wako aliyoyafanya siku ile, bwana wangu mfalme alipotoka Yerusalemu, bwana wangu mfalme asiyaweke moyoni! Kwani mtumwa wako anajua, ya kuwa mimi nimekosa; kwa hiyo unaniona leo, ya kuwa mimi ni wa kwanza wa mlango wote wa Yosefu, aliyeshuka kumwendea bwana wangu mfalme njiani. Ndipo, Abisai, mwana wa Seruya, alipojibu na kusema: Je? Simei asiuawe kwa ajili ya hayo tu? Kwani alimtukana aliyepakwa mafuta na Bwana. Lakini Dawidi akasema: Tuna bia gani mimi nanyi wana wa Seruya, mkitaka kuniwia leo Satani? Ingekuwaje, mtu akiuawa leo kwa Waisiraeli? Kwani si leo, nilipopata kujua, ya kuwa mimi ni mfalme wa Waisiraeli? Kisha mfalme akamwambia Simei na kumwapia: Hutauwa kabisa! Naye Mefiboseti, mwana wa Sauli, akashuka kumwendea mfalme njiani. Naye alikuwa hakuiogesha miguu yake, wala hakuzikata ndevu zake za midomoni, wala hakuzifua nguo zake tangu siku ile, mfalme alipokwenda, hata siku hiyo, aliporudi na kutengemana. Ikawa, alipotoka Yerusalemu kumwendea mfalme njiani, mfalme akamwuliza: Sababu gani hukuenda pamoja na mimi, Mefiboseti? Akasema: Bwana wangu mfalme, mtumishi wangu alinidanganya, kwani mtumishi wako alisema: Nitajitandikia punda, nimpande, nipate kwenda pamoja na mfalme, kwani mtumishi wako ni kiwete. Lakini yule amemsingizia mtumishi wako kwa bwana wangu mfalme, lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu, na ufanye yaliyo mema machoni pako! Kwani wao wote wa mlango wa baba yangu walikuwa watu wa kufa tu mbele ya bwana wangu mfalme, lakini wewe walimweka mtumishi wako kwao wanaokula mezani pako; liko jambo gani tena linipasalo, nimlilie tena mfalme kwa ajili yake? Mfalme akamwambia: Unayasemaje haya maneno yako tena? Basi, mimi ninatoa amri hii: Wewe na Siba mgawane mashamba! Ndipo, Mefiboseti alipomwambia mfalme: Na ayachukue yote yeye! Kwa kuwa bwana wangu mfalme amefika nyumbani kwake na kutengemana. Naye Barzilai wa Gileadi alikuwa ameshuka toka Roglimu, akapita naye mfalme kufika Yordani, apate kumvusha huko Yordani. Naye Barzilai alikuwa mzee mwenye miaka 80, naye ndiye aliyemtunza mfalme, alipokaa Mahanaimu, kwani alikuwa mtu mkuu sana. Mfalme akamwambia Barzilai: Wewe fuatana na mimi, nami nikutunze kwangu Yerusalemu! Lakini Barzilai akamwambia mfalme: Siku za miaka yangu ya kuwapo ni ngapi, nipande kwenda Yerusalemu pamoja na mfalme? Mimi ni mwenye miaka 80 leo, nitawezaje kupambanua yaliyo mema nayo yaliyo mabaya? Au mtumishi wako atawezaje kuuona utamu wa vilaji, ninavyovila, nao wa vinywaji, ninavyovinywa? Au nitawezaje kuzisikiliza sauti zao waimbaji wa kiume na wa kike? Kwa hiyo mtumishi wako atatakaje kukulemea tena, bwana wangu mfalme? Kidogo tu mtumishi wako atamsindikiza mfalme, akiisha kuuvuka Yordani. Sababu gani mfalme anataka kunirudishia tendo hili kwa njia ile? Mwache mtumishi wako, arudi, nipate kujifia mjini kwangu kwenye kaburi la baba yangu na la mama yangu. Lakini tazama, huyu ni mtumishi wako Kimuhamu; yeye atakwenda huko pamoja na bwana wangu mfalme, umfanyizie yaliyo mema machoni pako. Mfalme akajibu: Basi, Kimuhamu atakwenda huko pamoja na mimi, nami nitamfanyizia yaliyo mema machoni pangu, nayo yote, utakayonitakia, nitakufanyizia. Watu wote walipokwisha kuuvuka Yordani, mfalme naye akavuka; kisha mfalme akamnonea Barzilai, naye akambariki, kisha akarudi mahali pake. Mfalme alipoendelea kwenda Gilgali, Kimuhamu akaenda naye. Watu wote wa Yuda walikuwa wamevuka pamoja na mfalme, hata nusu ya watu wa Waisiraeli. Mara watu wote wa Waisiraeli wakaja kwa mfalme, wakamwambia mfalme: Mbona ndugu zetu Wayuda wamekuiba, wakimvusha mfalme nao wa mlango wako kule Yordani nao watu wote wa Dawidi waliokuwa naye. Ndipo, watu wote wa Yuda walipowajibu Waisiraeli: Maana mfalme ni karibu kwetu; kwa sababu gani mnalichafukia jambo hili? Je? Tumekula mali za mfalme? Au ametupa tunzo lo lote? Ndipo, Waisiraeli walipowajibu Wayuda kwamba: Mafungu yetu sisi yaliyoko kwa mfalme ni kumi, kwa hiyo naye Dawidi ni wetu kuliko wenu. Mbona mmetubeua? Je? Shauri hilo la kumrudisha mfalme halikutupasa kwanza sisi? Lakini maneno yao Wayuda yalikuwa magumu kuliko yao Waisiraeli. Ikatukia, ya kama kulikuwa na mtu asiyefaa, jina lake Seba, mwana wa Bikri, mtu wa Benyamini. Akapiga baragumu kwamba: Sisi hatuna fungu kwake Dawidi, wala hatuna lililo letu kwake mwana wa Isai. Ninyi Waisiraeli, kila mtu na aende hemani kwake. Ndipo, watu wote wa Waisiraeli walipopanda kwenda kwao wakiacha kumfuata Dawidi, ila wakamfuata Seba, mwana wa Bikri. Lakini Wayuda wakaandamana na mfalme wao toka mto wa Yordani hata mji wa Yerusalemu. Dawidi alipoingia nyumbani mwake huko Yerusalemu, mfalme akawachukua wale masuria kumi, aliowaweka kuiangalia nyumba, akawatia katika nyumba ya kulindwa, akawatunza humo, lakini hakuingia kwao. Basi, wakawa wafungwa mpaka siku ya kufa kwao, siku zao zikawa kama za wajane. Mfalme akamwambia Amasa: Waite watu wa Yuda, waje kwangu katika siku hizi tatu, kisha nawe uje kusimama hapa! Amasa akaenda kuwaita Wayuda; lakini alipokawia na kuupita muda, aliowekewa, Dawidi akamwambia Abisai: Sasa Seba, mwana wa Bikri, atatupatia mabaya kuliko Abisalomu; wewe wachukue watumishi wa bwana wako, umfukuze, asijipatie miji yenye maboma ya kuponea humo, macho yetu yasimwone tena. Ndipo, watu wa Yoabu walipotoka, wakamfuata nao Wakreti na Wapuleti na mafundi wote wa vita. Wakatoka Yerusalemu kwenda kumfukuza Seba, mwana wa Bikri. Wao walipofika kwenye lile jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akawatokea usoni. Naye Yoabu alikuwa amejifunga nguo zake za vitani, alizozivaa kila mara, juu yao alikuwa amejifunga upanga uliofungwa kiunoni, nao ulikuwa ndani ya ala yake; lakini alipokwenda huko na huko, ukaanguka. Yoabu akamwamkia Amasa kwamba: Hujambo, ndugu yangu? Kisha Yoabu akamshika Amasa udevu kwa mkono wake wa kulia, anoneane naye. Amasa asipouangalia upanga uliomo mkononi mwa Yoabu, akamchoma nao tumboni, matumbo yake yamwagike chini, hakumchoma mara ya pili, akafa tu. Kisha Yoabu na ndugu yake Abisai wakaenda kumfukuza Seba, mwana wa Bikri. Naye mmoja wao vijana wa Yoabu akaja kusimama kwake Amasa na kusema: Apendezwaye na Yoabu, naye aliye upande wa Dawidi na amfuate Yoabu! Lakini Amasa alikuwa anagaagaa katika damu yake katikati ya barabara; yule mtu alipoona, ya kuwa watu wote wanasimama hapo barabarani, akamwondoa Amasa hapo barabarani na kumtupa porini, kisha akamfunika kwa nguo, kwani aliona, ya kuwa kila aliyefika hapo alipo husimama. Alipokwisha kumwondoa hapo barabarani, watu wote wakapapita tu, waende kumfuata Yoabu, wamfukuze Seba, mwana wa Bikri. Huyo akapita kwa mashina yote ya Waisiraeli mpaka Abeli na Beti-Maka nao Haberimu wote; ndipo, watu walipokusanyika, wakaja kufuatana naye. Lakini wale walipokuja wakamsonga na kumzinga kule Abeli kwa Beti-Maka, wakiujengea mji huo boma la mchanga la kuuzunguka, nalo kikasimama papo hapo, mfereji wa boma la mji ulipokuwa. Nao watu wote waliokuwa na Yoabu wakachimba chini ya ukuta wa boma lao, wauangushe. Ndipo, mwanamke mwenye werevu wa kweli alipoita toka mjini kwamba: Sikieni! Sikieni! Mwambieni Yoabu, aje hapa karibu, niseme naye! Yoabu alipofika karibu yake, yule mwanamke akamwuliza: Wewe ndiwe Yoabu? Aliposema: Ndimi, akamwambia: Yasikilize maneno ya kijakazi wako! Akasema: Mimi nitayasikia. Akasema kwamba: Kale watu husema kwamba: Waulizeni watu wa Abeli! Ndivyo, walivyoyamaliza mashauri. Sisi tu Waisiraeli watulivu na welekevu, nawe unataka kuwaua watu wa humu mjini waliozaa makundi kwao Waisiraeli. Ni kwa nini, ukitaka kuwameza walio fungu lake Bwana? Yoabu akajibu kwamba: Hili linikalie mbali kabisa kwamba: Ninataka kumeza na kuangamiza! Hivi haviko kabisa, ila yuko mtoro wa milima ya Efuraimu, jina lake Seba, mwana wa Bikri; huyu ameuinua mkono wake, amwue mfalme Dawidi. Mtoeni huyu peke yake tu! Ndipo, nitakapoondoka penye mji huu. Naye yule mwanamke akamwambia Yoabu: Utakiona kichwa chake, kikitupwa kwako toka ukutani juu. Kisha huyu mwanamke akaja kuonana na watu wote na kuwatolea huo werevu wake wa kweli. Ndipo, walipokikata kichwa chake Seba, mwana wa Bikri, wakakitupia huko kwa Yoabu. Kisha akapiga baragumu, nao watu wakatawanyika wakiondoka kwenye ule mji, wakaenda kila mtu hemani kwake, naye Yoabu akarudi Yerusalemu kwa mfalme. Yoabu alikuwa mkuu wa vikosi vyote vya Waisiraeli, naye Benaya, mwana wa Yoyada, alikuwa mkuu wa Wakreti na wa Wapuleti. Naye Adoramu alikuwa mkuu wa kazi za nguvu, naye Yosafati, mwana wa Ahiludi, alikuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa. Naye Sewa alikuwa mwandishi, nao Sadoki na Abiatari walikuwa watambikaji. Naye Ira wa Yairi alikuwa mtambikaji wa Dawidi. Katika siku za Dawidi kulikuwa na njaa mwaka kwa mwaka, miaka mitatu; naye Dawidi alipoutafuta uso wa Bwana, Bwana akasema: Ziko manza za damu, Sauli nao wa mlango wake walizozikora walipowaua watu wa Gibeoni. Ndipo, mfalme alipowaita Wagibeoni kusema nao; nao Wagibeoni hawakuwa wana wa Isiraeli, ila walikuwa masao yao Waamori, nao wana wa Isiraeli walikuwa wamefanya maagano nao na kuapa, lakini Sauli alitaka kuwaua kwa kuona wivu kwa ajili ya wana wa Isiraeli na wa Yuda. Ndipo, Dawidi alipowauliza Wagibeoni: Niwafanyizie nini? Tena yale makosa niyalipe namna gani, mpate kuwabariki walio fungu lake Bwana? Wagibeoni wakamwambia: Sisi hatutaki fedha wala dhahabu kwake Sauli, wala kwao walio wa mlango wake, tena haitupasi kuua watu wa kwao Waisiraeli. Alipouliza tena: Mwasemaje? Niwafanyizie nini? wakamwambia mfalme: Yule mtu aliyetumaliza kwa kutaka kutuangamiza kabisa, tusikae tena katika mipaka yote ya Waisiraeli, basi, na tupewe wanawe saba, tuwanyonge machoni pa Bwana kule Gibea kwa Sauli aliyekuwa mteule wa Bwana. Mfalme akawaambia: Mimi nitawapa. Mfalme akamhurumia Mefiboseti, mwana wa Yonatani, mwana wa Sauli, kwa ajili ya kiapo, alichokiapa na kumtaja Bwana, awe shahidi wao, yeye Dawidi naye Yonatani, mwana wa Sauli. Kwa hiyo mfalme akachukua wana wawili wa Risipa, binti Aya, aliomzalia Sauli, ndio Armoni na Mefiboseti, na wana watano wa Mikali, binti Sauli aliomzalia Adirieli, mwana wa Barzilai wa Mehola. Akawatia mikononi mwa Wagibeoni, nao wakawanyonga mlimani juu machoni pa Bwana; nao wote saba wakauawa pamoja; walipouawa, ni siku za kwanza za mavuno, watu walipoanza kuvuna mawele. Kisha Risipa, binti Aya, akachukua gunia, akalitandika la kulalia mwambani juu tangu hapo, watu walipoanza kuvuna, mpaka mvua zitokazo mbinguni zikawanyeshea wale wafu, hakuacha ndege wa angani kuwakalia mchana, wala nyama wa porini kuwafikia usiku. Dawidi alipopashwa habari za mambo hayo, Risipa, binti Aya, suria yake Sauli, aliyoyafanya, Dawidi akaenda akaichukua mifupa ya Sauli nayo mifupa ya mwanawe Yonatani kwa wenyeji wa Yabesi wa Gileadi walioiiba uwanjani kwa Beti-Sani; ndiko, Wafilisti walikoitungika siku hiyo, Wafilisti walipomwua Sauli huko Gilboa. Alipoichukua huko mifupa ya Sauli na mifupa ya mwanawe Yonatani, wakaikusanya nayo mifupa yao hao walionyongwa, wakaizika mifupa ya Sauli nayo ya mwanawe Yonatani katika nchi ya Benyamini kule Sela kaburini kwa baba yake Kisi. Walipokwisha kuyafanya yote, mfalme aliyoyaagiza, baadaye Mungu akasikia alipoombwa kwa ajili ya nchi hiyo. Baadaye Wafilisti walipokuja tena kupigana na Waisiraeli, Dawidi akashuka pamoja na watumishi wake. Walipopigana na Wafilisti, Dawidi akachoka. Ndipo, alipotokea Isibi-Benobu aliyekuwa mmoja wao yale Majitu marefu; huyu alikuwa na mkuki wenye ncha ya shaba, nayo ilipopimwa, uzito wake ulikuwa sekeli 300, ndio nusu ya frasila; naye alikuwa amejifunga mata mapya, akataka kumwua Dawidi. Ndipo, Abisai, mwana wa Seruya, alipomsaidia na kumpiga yule Mfilisti, hata akafa. Hapo ndipo, watumishi wa Dawidi walipomwapia kwamba: Wewe hutatoka tena pamoja na sisi kwenda vitani, usiizime taa ya waisiraeli! Hayo yalipokwisha yakawa mapigano mengine nao Wafilisti kule Gobu; ndiko, Sibekai wa Husa alikomwua Safu aliyekuwa naye mmoja wao yale Majitu marefu. Kisha kule Gobu yakawa mapigano mengine na Wafilisti; ndiko, Elihanani wa Beti-Lehemu, mwana wa Yare-Orgimu, alikomwua Goliati wa Gati; huyu uti wa mkuki wake ulikuwa kama majiti ya wafuma nguo. Kisha yakawa mapigano tena kule Gati; huko kulikuwa na mtu mrefu sana, vidole vya mikono yake na vidole vya miguu yake vilikuwa sita sita, vyote pamoja ni 24, naye alikuwa amezaliwa kwao yale Majitu marefu. Alipowatukana Waisiraeli, Yonatani, mwana wa Simea, kaka yake Dawidi, akamwua. Hawa wanne walizaliwa Gati kwao yale Majitu marefu, wakauawa kwa mikono ya Dawidi na kwa mikono ya watumishi wake. Dawidi akamwambia Bwana maneno ya wimbo huu, Bwana alipomponya mikononi mwa adui zake wote, namo mikononi mwa Sauli. Akasema: Bwana ni ngome yangu na boma langu, tena mponya wangu; ni Mungu aliye mwamba wangu, kwa hiyo ninamjetea, ni ngao yangu na pembe yangu ya kunipatia wokovu, kisha ni kingo langu, nipate pa kukimbilia, ni mwokozi wangu aniokoaye, nisije kukorofishwa. Bwana atukuzwaye ndiye, ninayemwitia; ndipo, ninapookolewa mikononi mwao walio adui zangu. Kwani mafuriko ya maji yauayo yalikuwa yameniasamia, nayo majito yaangamizayo yalinistusha, kamba zivutiazo kuzimuni zilikuwa zimenizunguka, nayo mafungo yauayo yalikuwa mbele yangu. Hapo niliposongeka nalimwita Bwana, yeye aliye Mungu wangu nikamlalamikia, akaisikia sauti yangu Jumbani mwake, malamamiko yangu yakamwingia masikioni mwake. Nchi ikatukutika na kutetemeka, nayo misingi ya mbingu ikatikisika kwa kutukuswa, kwani aliitolea makali yake yenye moto. Moshi ukapanda puani mwake, moto ulao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yakamulikamulika mbele yake. Akatanda mbingu ya kushukiapo, mawingu meusi yakawa chini ya miguu yake. Akapanda gari, nalo likarushwa, akaonekana mabawani mwa upepo. Akatumia giza kuwa kao, limfunike pande zote, ndio mawingu yenye mvua kali na kimbunga. Kwa nguvu ya kumulika mbele yake yakawashwa makaa ya moto. Bwana akapiga ngurumo kule mbinguni, Alioko huko juu akaivumisha sauti yake. Alipopiga mishale, akawatawanya, ngurumo zilipozidi, wakapigwa bumbuazi. Ndipo, vilipoonekana vilindi vya baharini, nayo misingi ya nchi ikafunuliwa kwa nguvu ya makaripio yake yeye Bwana na kwa ukali wa pumzi ya pua yake. Akakunjua mkono toka juu, akanikamata, mle mlimo na maji mengi akanichopoa. Akaniponya mikononi mwa adui yangu mwenye nguvu namo mwao walionichukia kwa kuwa na uwezo kuliko mimi. Walikuwa wamenijia mbele ile siku, nilipokuwa nimeshindwa, lakini Bwana akanijia kuwa shikizo. Akanitoa kwao, akanikalisha palipo papana; ndivyo, alivyoniopoa kwa kupendezwa nami. Bwana alinipa yaupasayo wongofu wangu, akanipatia tena yaupasayo ung'avu wa mikono yangu. Kwani naliziangalia njia zake Bwana, nisifanye kilicho kiovu mbele yake Mungu wangu. Kwani maamuzi yake yote yako mbele yangu, nayo maongozi yake sikuacha kuyafuata. Nikawa wake pasipo kuonywa, nikajiangalia, nisimkosee. Bwana akanipatia tena yaupasayo wongofu wangu, kwa kuwa nilikuwa nimeng'aa machoni pake. Wewe humwia mpole aliye mpole, naye aliye mkweli wote nawe humwia mkweli wote. Wewe humwia mng'avu aliye mng'avu, lakini aliye mpotovu nawe humpotokea. Walio wanyonge huwaokoa, lakini macho yako huwapingia wajivunao, uwanyenyekeze. Kwani wewe, Bwana, u taa yangu, naye Bwana huliangaza nalo giza langu. Kwani nitashambulia vikosi vizima kwa nguvu yako, kwa nguvu ya Mungu wangu narukia napo ukutani. Njia yake Mungu haipindiki, Neno lake Bwana limeng'azwa, yeye ni ngao yao wote wamkimbiliao. Kwani yuko nani aliye Mungu, asipokuwa Bwana? Tena yuko nani aliye mwamba, asipokuwa Mungu wetu? Mungu ni ngome yangu yenye nguvu, njia yangu huifanya po pote, iwe imenyoka kabisa. Hunipatia miguu ikimbiayo kama ya kulungu, anisimamishe kwangu vilimani juu. Huifundisha mikono yangu kupiga vita, mpaka mikono yangu iweze kupinda hata uta wa shaba. Hunipa ngao ya kuniokoa, napo hapo, unaponinyenyekeza, hunikuza. Huipanulia miguu yangu, ipate pa kupitia, viwiko vya miguu yangu visiteleze. Na niwakimbize adui zangu, mpaka niwaangamize; sitarudi nisipokwisha kuwamaliza. Nitawamaliza na kuwaponda, wasiinuke tena, sharti waanguke miguuni pangu. Hunivika nguvu ya kupiga vita, huwalaza chini yangu wao waniinukiao. Hunipa adui zangu, niwaone migongo, nipate kuwanyamazisha wachukivu wangu. Hakuna mwokozi, wanapolalamika, wanapomwitia Bwana, hawaitikii. Nitawaponda, mpaka wabunguke kama mavumbi ya nchi, nikiisha kuwaseta, niwazoe kama mataka viwanjani. Kwenye magomvi yao walio ukoo wangu ulinitoa, ukaniangalia, nipate kuwa kichwa chao wao wamizimu, watu, ambao nilikuwa siwajui, wanitumikie. Hao watokao mbali hunipongeza, masikio yao yanaponisikia, hunitii. Hao watokao mbali walikuwa wamenyauka walipotoka mabomani kwao na kutetemeka. Bwana Mwenye uzima ni mwamba wangu upasao kusifiwa, yeye Mungu wa mwamba wangu aliyeniokoa sharti atukuke! Mungu ndiye aliyenipatia malipizi na kushurutisha makabila ya watu, wanitii, Ndiye aliyenitoa mikononi mwao walio adui zangu, kwao waniinukiao ukaniweka kuwa mkuu wao, kwao waliozidi kunikorofisha ukaniponya. Kwa hiyo nitakushukuru, Bwana, kwenye wamizimu, nalo Jina lako nitaliimbia. Mfalme wake alimpatia wokovu mwingi, aliyempaka mafuta humfanyizia yenye upole; huyo ni Dawidi naye aliye uzao wake kale na kale. Haya ndiyo maneno ya mwisho ya Dawidi: Hivyo ndivyo, asemavyo Dawidi, mwana wa Isai, haya ndiyo, aliyoyasema mtu aliyetukuka sana, Mungu wa Yakobo alimpaka mafuta, kwa kuwatungia Waisiraeli nyimbo alipendeza. Roho ya Bwana hunitumia kuwa wa kusema, Neno lake limo kinywani mwangu. Mungu wa Isiraeli aliniambia neno, aliye mwamba wa Waisiraeli alisema kwamba: Awatawalaye watu kwa wongofu, awatawalaye kwa kumcha Mungu, hufanana na mwanga wa asubuhi, jua linapokucha, huwa kama mapema ya asubuhi yasiyo na mawingu, majani mabichi huchipuka nchini, mvua ikiisha kuanuka; ni kwa nguvu za kuangaza kwake, vikiwa hivyo. Kumbe sivyo, mlango wangu ulivyo kwake Mungu? Kwani aliniwekea agano kuwa la kale na kale, lilitengenezwa, yote yawe sawa, lipate kuangaliwa. Kwa hiyo asiyachipuze yote yawezayo kuniokoa, nayo yote pia yapendezayo? Lakini wao wote wasiofaa ni kama miiba inayotupwa tu, kwani haishikiki mikononi mwa watu. Mtu atakaye kuwajia hutumia vyuma tele na uti wa mkuki, kisha huteketezwa kwa moto papo hapo, walipokuwa. Haya ndiyo majina ya mafundi wa vita, Dawidi alio kuwa nao: Yosebu-Basebeti wa Takemoni, mkuu wa thelathini; yeye aliuchezesha mkuki wake juu ya watu 800; ndio, aliowaua kwa mara moja. Aliyemfuata ni Elazari, mwana wa Dodo, mwana wa mtu wa Ahohi; huyu alikuwa mmoja wao wale mafundi wa vita watatu waliokuwa na Dawidi, Wafilisti walipowatukana na kujipanga huko kupigana nao. Watu wa Waisiraeli walipokwenda zao mahali pa juu, yeye akainuka, akawapiga Wafilisti, mpaka mkono wake ukimlegea kwa kugandamana na upanga. Ilikuwa siku hiyo, Bwana alipowapatia wokovu mkubwa, kisha watu wakarudi na kumfuata, wateke nyara. Aliyefuata ni Sama, mwana wa Age, wa Harari. Wafilisti walipokusanyika wengi mno mahali palipokuwa na kipande cha shamba lenye kunde, watu wakawakimbia Wafilisti; ndipo, yeye alipokuja kusimama katikati ya hicho kipande cha shamba, akakiponya akiwapiga Wafilisti. Ndivyo, Bwana alivyowapatia wokovu mkubwa. Ikawa, hawa wakuu watatu waliomo miongoni mwao wakuu wa 30 wakashuka siku za mavuno, wafike kwa Dawidi penye pango la Adulamu; navyo vikosi vya Wafilisti vilikuwa vimepiga makambi Bondeni kwa Majitu. Naye Dawidi siku zile alikuwa ngomeni, nacho kikosi cha walinzi wa Wafilisti kilikuwamo Beti-Lehemu. Hapo Dawidi akaingiwa na tamaa, akasema: Yuko nani atakayeninywesha maji ya kisima cha Beti-Lehemu kilichoko langoni? Ndipo, wale mafundi wa vita watatu walipojipenyeza makambini mwa Wafilisti, wakachota maji katika kisima cha Beti-Lehemu kilichoko langoni, wakayachukua, wakamletea Dawidi, lakini hakutaka kuyanywa, akammwagia Bwana kuwa kinywaji cha tambiko, akasema: Bwana na anizuie, nisifanye kama hayo! Kumbe siyo damu za waume hao waliokwenda kwa kujitoa wenyewe? Kwa hiyo hakutaka kuyanywa. Haya waliyafanya wale mafundi wa vita watatu. Naye Abisai, ndugu yake Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu miongoni mwa watu watatu; yeye ndiye aliyeuchezesha mkuki wake juu ya watu 300; ndio, aliowaua, akawa mwenye macheo kwa hao watatu. Kwao hao watatu aliheshimiwa kweli kuliko wengine, akawa mkuu wao, lakini wale watatu wa kwanza hakuwa sawa nao. Benaya, mwana wa Yoyada, mwana wa mtu mwenye nguvu, alifanya matendo makuu, nako kwao kulikuwa Kabuseli. Yeye aliwaua wana wawili wa Arieli wa Moabu, tena siku moja, theluji ilipokuwa imeanguka, akashuka shimoni, akaua simba mlemle. Naye ndiye aliyemwua mtu wa Misri aliyetisha kwa kutazamwa tu; namo mkononi mwake huyu Mmisri alishika mkuki. Lakini akamshukia na kushika fimbo tu, akampokonya yule Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa huo mkuki wake. Haya aliyafanya Benaya, mwana wa Yoyada, kwa hiyo alipata macheo kwa hao mafundi wa vita watatu. Kwa wale 30 aliheshimiwa kuliko wenziwe, lakini wale watatu wa kwanza hakuwa sawa nao. Naye Dawidi akamweka kuwa mkuu wa walinzi wake. Miongoni mwao wakuu wa 30 walikuwa: Asaheli, ndugu yake Yoabu; Elihanani, mwana wa Dodo wa Beti-Lehemu; Sama wa Harodi, Elika wa Harodi; Helesi wa Palti, Ira, mwana wa Ikesi, wa Tekoa; Abiezeri wa Anatoti, Mebunai wa Husa; Salmoni wa Ahohi, Maharai wa Netofa; Helebu, mwana wa Baana, wa Netofa, Itai, mwana wa Ribai, wa Gibea wa wana wa Benyamini; Benaya wa Piratoni, Hidai wa Nahale-Gasi; Abi-Alboni wa Araba, Azimaweti wa Barihumu; Eliaba wa Salaboni, Yonatani wa wana wa Yaseni; Sama wa Harari, Ahiamu, mwana wa Sarari, wa Arari; Elifeleti, mwana wa Ahasibai, mwana wa mtu wa Maka, Eliamu, mwana wa Ahitofeli, wa Gilo; Hesirai wa Karmeli, Parai wa Arabu; Igali, mwana wa Natani wa Soba, Bani wa Gadi; Mwamoni Seleki, Naharai wa Beroti aliyekuwa mchukua mata wa Yoabu, mwana wa Seruya; Mwitiri Ira, Mwitiri Garebu; Mhiti Uria. Wote pamoja ni 37. Makali ya Bwana yakawawakia Waisiraeli tena, kwa hiyo akamhimiza Dawidi kuwaponza akimwambia: Wahesabu Waisiraeli na Wayuda! Ndipo, mfalme alipomwambia Yoabu, mkuu wa vikosi aliyekuwa naye: Zunguka katika mashina yote ya Waisiraeli toka Dani mpaka Beri-Seba, mwahesabu watu, nipate kuzijua hesabu za watu. Yoabu akamwambia mfalme: Bwana Mungu wako na aendelee kuwaongeza watu vivyo hivyo mara mia, naye bwana wangu mfalme na ayaone kwa macho yake! Lakini neno hilo bwana wangu mfalme analitakia nini? Lakini neno la mfalme likapata nguvu, asimsikie Yoabu wala wakuu wa vikosi; ndipo, Yoabu alipotoka na wakuu wa vikosi machoni pa mfalme kwenda kuwahesabu watu wa Waisiraeli. Walipokwisha kuuvuka Yordani wakapiga kambi kule Aroeri kuumeni kwa mji ulioko katikati ya Bonde la Gadi kuelekea Yazeri. Kisha wakafika Gileadi na nchi ya Tatimu-Hodisi, kisha wakafika Dani-Yani, wakazunguka kwenda Sidoni. Kisha wakafika katika boma la Tiro, hata miji yote ya Wahiti na ya Wakaanani wakaiingia, kisha wakatoka kwenda kusini kuingia Yuda mpaka Beri-Seba. Walipokwisha kuzunguka katika nchi zote, wakafika Yerusalemu, miezi 9 na siku 20 zilipokwisha pita. Ndipo, Yoabu alipompa mfalme jumla ya hesabu za watu: Waisiraeli wenye nguvu wanaoweza kushika panga walikuwa watu 800000, nao Wayuda watu 500000. Dawidi alipokwisha kuwahesabu watu, moyo ukampiga; ndipo, Dawidi alipomwambia Bwana: Nimekosa sana kwa kulifanya hilo. Sasa Bwana, umwondolee mtumishi wako hizo manza, nilizozikora! Kwani nimefanya kisichopasa kabisa. Dawidi alipoamka kesho yake, neno la Bwana likamjia mfumbuaji Gadi aliyekuwa mchunguzaji wa Dawidi, kwamba: Nenda kumwambia Dawidi: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mimi ninakuwekea mambo matatu, ndimo uchague moja lao, nikufanyizie. Gadi akaja kwa Dawidi, akampasha hiyo habari na kumwuliza: Ikujie katika nchi yako miaka saba ya njaa? Au ukimbizwe miezi mitatu nao wakusongao, wakikufuata upesiupesi? Au uwe siku tatu katika nchi yako ugonjwa mbaya uuao? Sasa yawaze moyoni, uone nitakayomjibu aliyenituma. Dawidi akamwambia Gadi: Nimesongeka sana, lakini na nijitupe mkononi mwake Bwana, kwani huruma zake ni nyingi, nisijitupe mikononi mwa watu. Ndipo, Bwana alipowauguza Waisiraeli ugonjwa mbaya uuao tangu asubuhi, mpaka utimie muda, aliouweka. Toka Dani mpaka Beri-Seba wakafa kwao walio wa ukoo huo watu 70000. Malaika alipoukunjua mkono wake kuuangamiza Yerusalemu, Bwana akageuza moyo kwa ajili ya huo ubaya, akamwambia yule malaika aliyewaangamiza watu: Sasa inatosha, ulegeze mkono wako! Naye yule malaika wa Bwana alikuwa penye kupuria ngano pa Myebusi Arauna. Dawidi alipomwona yule malaika, jinsi alivyowapiga watu, akamwambia Bwana kwamba: Tazama, mimi nimekosa, mimi nimekora manza; lakini hawa kondoo wamefanya nini? Kwa hiyo mkono wako na unipige mimi na mlango wa baba yangu. Siku hiyo Gadi akaja kwake Dawidi, akamwambia: Mtengenezee Bwana pa kutambikia penye kupuria ngano pa Myebusi Arauna! Kwa hilo neno la Gadi Dawidi akapanda, kama Bwana alivyoagiza. Arauna alipochungulia akamwona mfalme na watumishi wake, wakipanda kuja kwake; ndipo, Arauna alipotoka, akamwangukia mfalme usoni pake hapo chini. Kisha Arauna akauliza: Ni kwa sababu gani, bwana wangu mfalme akija kwa mtumishi wake? Dawidi akamwambia: Ninataka kununua kwako hapa pako pa kupuria ngano, nijenge pa kumtambikia Bwana, huku kuuawa kwa watu kukomeshwe. Arauna akamwambia Dawidi: Bwana wangu mfalme na apachukue tu, atambike, kama yalivyo mema machoni pake. Tazama, nakupa hawa ng'ombe kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, nayo haya magari na vyombo vya ng'ombe nakupa kuwa kuni. Haya yote, mfalme, Arauna anampa mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme: Bwana Mungu wako na apendezwe na wewe! Lakini mfalme akamwambia Arauna: Sivyo, ila nitapanunua kabisa kwako na kulipa kilicho kiasi chake; sitamtolea Bwana Mungu wangu ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, nisizozilipa. Kisha Dawidi akapanunua hapo pa kupuria pamoja na ng'ombe kwa fedha 50. Kisha Dawidi akamjengea Bwana hapo mahali pa kumtambikia, akamtolea ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na vipaji vya tambiko vya kumshukuru. Ndipo, Bwana aliposikia akiombwa kwa ajili ya nchi hiyo, nako kuuawa kwao Waisiraeli kukakomeshwa. Mfalme Dawidi alipokuwa mzee kwa kuendelea sana kuwa mwenye siku nyingi, wakamfunika kwa nguo, lakini hakupata joto. Ndipo, watumishi wake walipomwambia: Sharti wamtafutie bwana wetu mfalme kijana aliye mwanamwali wa kusimama mbele ya mfalme na kumtunza. Naye akilala kifuani pako, bwana wetu mfalme, utapata joto. Wakatafuta msichana aliyekuwa mzuri kuwashinda wengine waliokuwa mipakani kwa Waisiraeli, wakamwona Abisagi wa sunemu, wakampeleka kwake mfalme. Huyu msichana alikuwa mzuri mno, akawa mtunzaji wa mfalme, akamtumikia, lakini mfalme hakumjua. Naye Adonia, mwana wa Hagiti, akajikweza kwamba: Mimi nitakuwa mfalme, akajipatia magari na farasi na watu 50, wamtangulie kwa kupiga mbio. Lakini baba yake hakumsikitisha tangu siku zake za kale kwamba: Mbona unafanya kama hayo? Naye kwa kutazamwa alikuwa mtu mzuri mno, naye mama yake alimzaa baada ya Abisalomu. Akapiga shauri na Yoabu, mwana wa Seruya, tena na mtambikaji Abiatari, wakamsaidia kwa kurudi upande wake Adonia. Lakini mtambikaji Sadoki na Benaya, mwana wa Yoyada, na mfumbuaji Natani na Simei na Rei na mafundi wa vita wa Dawidi hawakuwa upande wake Adonia. Kisha Adonia akatambika penye Jiwe la Zoheleti (Mwamba wa Nyoka) karibu na Eni-Rogeli (Chemchemi ya Wafua nguo) na kuchinja kondoo na ng'ombe na vinono, akawaalika ndugu zake wote waliokuwa wana wa mfalme wa waume wote wa Yuda waliomtumikia mfalme. Lakini mfumbuaji Natani na Benaya nao mafundi wa vita naye ndugu yake Salomo hakuwaalika. Ndipo, Natani alipomwambia Bati-Seba, mamake Salomo, kwamba: Hukusikia, ya kuwa Adonia, mwana wa Hagiti, amejipa ufalme, bwana wetu Dawidi asivijue? Sasa nitakupa shauri upate kujiponya mwenyewe pamoja na roho yake mwanao Salomo. Nenda, uingie mwake mfalme Dawidi, umwambie: Je? Wewe, bwana wangu mfalme, hukumwapia kijakazi wako kwamba: Mwanao Salomo atakuwa mfalme nyuma yangu, yeye akae katika kiti changu cha kifalme? Mbona Adonia amekwisha kujipa ufalme? Ukiwa hujamaliza bado kusema mle na mfalme, utaniona mimi, nikiingia nyuma yako, niyamalize maneno yako. Ndipo, Bati-Seba alipoingia chumbani mwake mfalme, naye mfalme alikuwa mzee sana, naye Abisagi wa Sunemu alimtumikia mfalme. Bati-Seba akainama na kumwangukia mfalme; mfalme akamwuliza: Una nini? Akamwambia: Bwana wangu, wewe ulimwapia kijakazi wako na kumtaja Bwana Mungu wako kwamba: Mwanao Salomo atakuwa mfalme nyuma yangu, yeye akae katika kiti changu cha kifalme. Lakini sasa tazama, Adonia amekwisha kujipa ufalme, nawe bwana wangu mfalme huvijui! Akatambika na kuchinja ng'ombe na vinono na kondoo wengi, akawaalika wana wote wa mfalme na mtambikaji Abiatari na Yoabu, mkuu wa vikosi, lakini mtumwa wako Salomo hakumwalika. Nawe, bwana wangu mfalme, macho ya Waisiraeli wote yanakuelekea wewe, uwaambie, kama ni nani atakayekaa katika kiti cha kifalme cha bwana wangu mfalme nyuma yake. Hivyo itakuwa, bwana wangu mfalme atakapolala na baba zake, mimi na mwanangu Salomo tuwe wakosaji. Alipokuwa akisema bado na mfalme, mara mfumbuaji Natani akaja. Wakamwambia mfalme kwamba: Mfumbuaji Natani amekuja. Alipokuja mbele ya mfalme, akamwangukia mfalme na kuufikisha uso wake chini. Kisha Natani akasema: Bwana wangu mfalme, umesema: Adonia awe mfalme nyuma yangu, naye akae katika kiti changu cha kifalme? Kwani siku hii ya leo ameshuka, akatambika na kuchinja ng'ombe na vinono na kondoo wengi, akaalika wana wote wa mfalme na wakuu wa vikosi na mtambikaji Abiatari, nao wamo katika kula na kunywa mbele yake wakisema: Pongezi, mfalme Adonia! Lakini mimi niliye mtumwa wako na mtambikaji Sadoki na Benaya, mwana wa Yoyada, na mtumwa wako Salomo hakutualika. Inakuwaje? Neno hilo limetoka kwako, bwana wangu mfalme, usimjulishe mtumwa wako, kama ni nani atakayekaa katika kiti cha kifalme cha bwana wangu mfalme nyuma yake? Mfalme Dawidi akajibu akisema: Niitieni Bati-Seba! Alipokuja mbele ya mfalme na kusimama mbele ya mfalme, ndipo, mfalme alipoapa akisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyeiokoa roho yangu katika masongano yote, siku hii ya leo nitavifanya, nilivyokuapia na kumtaja Bwana Mungu wa Isiraeli kwamba: Mwanao Salomo atakuwa mfalme nyuma yangu, yeye akae katika kiti changu cha kifalme mahali pangu. Bati-Seba akauinamisha uso chini, akamwangukia mfalme akisema: Bwana wangu mfalme Dawidi na awepo uzimani kale na kale! Kisha mfalme Dawidi akasema: Niitieni mtambikaji Sadoki na mfumbuaji Natani na Benaya, mwana wa Yoyada! Walipokuja mbele ya mfalme, mfalme akawaambia: Wachukueni watumishi wa bwana wenu kwenda nanyi, mkimpandisha mwanangu Salomo katika nyumbu wangu mimi, mmtelemshe huko Gihoni! Huko mtambikaji Sadoki na mfumbuaji Natani wampake mafuta, awe mfalme wa Waisiraeli. Kisha mtapiga mabaragumu kwamba: Pongezi, mfalme Salomo! Baadaye mtampandisha kufika huku, aje kukaa katika kiti changu cha kifalme, yeye awe mfalme mahali pangu. Yeye ndiye, niliyemwagiza kuwa mtawalaji wa Waisiraeli na wa Wayuda. Benaya, mwana wa Yoyada, akamwitikia mfalme akisema: Amin. Naye Bwana Mungu wa bwana wangu mfalme na aseme hivyo! Kama Bwana alivyokuwa na bwana wangu mfalme, vivyo hivyo na awe naye Salomo akikikuza kiti chake cha kifalme kuliko kiti cha kifalme cha bwana wangu mfalme Dawidi! Mtambikaji Sadoki na mfumbuaji Natani na Benaya, mwana wa Yoyada, na Wakreti na Wapuleti wakashuka, wakampandisha Salomo katika nyumbu wa mfalme Dawidi, wakampeleka Gihoni. Naye mtambikaji Sadoki alikuwa ameichukua pembe ya mafuta mle Hemani, akampaka Salomo mafuta; ndipo, walipopiga mabaragumu, nao watu wote wakasema: Pongezi, mfalme Salomo! Kisha watu wote pia wakapanda na kumfuata wakipiga filimbi kwa kufurahi furaha kubwa, hata nchi ikavuma kwa sauti zao kuu. Adonia nao watu walioalikwa naye waliokuwa naye walipovisikia walikuwa wamekwisha kula. Yoabu alipozisikia sauti za mabaragumu akauliza: Makelele na mavumo ya mjini ni ya nini? Alipokuwa akisema bado, mara akaja Yonatani, mwana wa mtambikaji Abiatari; Adonia akamwambia: Njoo! Kwani wewe u mtu mwenye nguvu, utatuletea habari njema. Lakini Yonatani akajibu akimwambia Adonia: Sivyo! Bwana wetu mfalme Dawidi amempa Salomo kuwa mfalme! Mfalme akatuma pamoja naye mtambikaji Sadoki na mfumbuaji Natani na Benaya, mwana wa Yoyada, na Wakreti na Wapuleti, wakampandisha katika nyumbu wa mfalme. Mtambikaji Sadoki na mfumbuaji Natani wakampaka mafuta kule Gihoni, awe mfalme, kisha wakapanda kutoka huko wenye furaha, mji ukavuma; hizo ndizo sauti, mlizozisikia. Kisha Salomo akapata hata kukaa katika kiti cha kifalme. Hata watumishi wa mfalme wamekwisha kwenda kumpongeza bwana wetu mfalme Dawidi wakisema: Mungu wako na alitukuze jina la Salomo kuliko jina lako! Tena kiti chake cha kifalme na akikuze kuliko kiti chako cha kifalme! Ndipo, mfalme alipojiinamisha kitandani pake, naye mfalme akasema kama haya: Bwana Mungu wa Isiraeli na atukuzwe, kwa kuwa leo amemtoa atakayekaa katika kiti changu cha kifalme, macho yangu yakiviona! Ndipo, wote walioalikwa waliokuwa kwake Adonia waliposhikwa na woga, wakaondoka, wakajiendea, kila mtu akishika yake njia. Adonia akamwogopa Salomo, akaondoka, akaenda, akazishika pembe za meza ya Bwana. Salomo akapashwa habari kwamba: Tazama, Adonia anamwogopa mfalme Salomo! Tazama, amezishika pembe za meza ya Bwana akisema: Mfalme Salomo sharti aniapie leo, asimwue mtumwa wake kwa upanga! Salomo akasema: Kama atakuwa mtu mwelekevu, unywele wake mmoja tu hautaanguka chini; lakini ukionekana ubaya kwake, atakufa. Mfalme Salomo akatuma, wamshushe penye meza ya Bwana; ndipo, alipokuja, akamwangukia mfalme Salomo, Salomo akamwambia: Nenda nyumbani mwako! Siku za kufa kwake Dawidi zilipofika karibu, akamwonya mwanawe Salomo akisema: Mimi sasa ninakwenda njia inayowapasa wote wa huku nchini; nawe jipe moyo, uwe mtu wa kiume! Yaangalie mambo ya Bwana Mungu wako, ayatakayo, yaangaliwe, ukizishika njia zake na kuyaangalia maongozi yake na maagizo yake na maamuzi yake na mashuhuda yake, kama yalivyoandikwa katika Maonyo ya Mose. Ndivyo, utakavyofanikiwa katika matendo yako yote po pote, utakapojielekezea. Hivyo ndivyo, naye Bwana atakavyolitimiza neno lake, aliloniambia kwamba: Wanao watakapoziangalia njia zao, waendelee mbele yangu kikweli kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, basi, kwako hakutakoseka mtu atakayekaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli. Wewe nawe unayajua, Yoabu, mwana wa Seruya, aliyonifanyizia, nayo, aliyowafanyizia wale wakuu wawili wa vikosi vya Waisiraeli, Abineri, mwana wa Neri, na Amasa, mwana wa Yeteri, akiwaua na kulipiza damu za vita siku za utengemano, hizo damu za vita akazimwagia mshipi wake, aliouvaa viunoni mwake, navyo viatu vyake, alivyovivaa miguuni pake. Umfanyizie kwa werevu wako ulio wa kweli usipoacha, mvi zake zishuke kuzimuni na kutengemana. Lakini wana wa Barzilai wa Gileadi uwafanyizie vema, wawe miongoni mwao wanaokula mezani pako. Kwani hivyo ndivyo, walivyonijia mimi, nilipomkimbia ndugu yako Abisalomu. Tena tazama, unaye Simei, mwana wa Gera, aliye mtu wa Benyamini wa Bahurimu; ameniapiza kwa kiapo kibaya zaidi siku ile, nilipokwenda Mahanaimu. Naye halafu aliposhuka kuniendea huko Yordani, nikamwapia na kumtaja Bwana kwamba: Sitakuua kwa upanga. Sasa wewe usimwache kuwa kama mtu asiyekosa! Kwani wewe ndiwe mtu mwerevu wa kweli, utayajua, utakayomfanyizia, uzitelemshe mvi zake kuzimuni, zikiwa zenye damu. Kisha Dawidi akalala na baba zake, akazikwa mjini mwa Dawidi. Nazo siku, Dawidi alizokuwa mfalme wa Waisiraeli, ni miaka 40; Heburoni alishika ufalme miaka 7, namo mle Yerusalemu alishika ufalme miaka 33. Salomo akakaa katika kiti cha kifalme cha baba yake Dawidi, nao ufalme wake ukapata kushupaa sana. Adonia, mwana wa Hagiti, akaja kwa Bati-Seba, mamake Salomo, naye akamwuliza: Kuja kwako ni kwema? Akajibu: Ndio, ni kwema. Kisha akasema: Nina neno la kusema na wewe; akamwambia: Liseme! Akasema: Unajua, ya kuwa ufalme ulikuwa wangu, nao Waisiraeli wote walikuwa wakinielekezea nyuso zao, niwe mfalme; lakini tena ufalme ukageuka kuwa wa ndugu yangu, kwani ulikuwa wake kwa agizo la Bwana. Sasa mimi ninaomba kwako ombo moja, nawe usiutweze uso wangu! Akamwambia: Sema! Akasema: Sema na mfalme Salomo, kwani hatautweza uso wako, anipe Abisagi wa Sunemu, awe mke wangu. Bati-Seba akasema: Basi, mimi nitakusemea kwake mfalme. Bati-Seba alipokuja kwa mfalme Salomo kumsemea Adonia kwake, mfalme akaondoka na kumwendea njiani, akamwinamia, kisha akakaa katika kiti chake cha kifalme; kisha mfalme akamwekea mama yake kiti cha kifalme, akakaa kuumeni kwake. Kisha akasema: Mimi ninakuomba ombo moja lililo dogo, nawe usiutweze uso wangu! Mfalme akamwambia: Omba, mamangu! Kwani sitautweza uso wako. Akasema: Ndugu yako Adonia na apewe Abisagi wa Sunemu, awe mkewe. Mfalme Salomo akajibu akimwambia mama yake: Ni kwa sababu gani, ukimwombea Adonia, apewe Abisagi wa Sunemu? Umwombee nao ufalme! Kwani yeye ni ndugu yangu aliye mkubwa kuliko mimi. Waombee nao akina mtambikaji Abiatari na Yoabu, mwana wa Seruya! Kisha mfalme Salomo akaapa na kumtaja Bwana akisema: Mungu na anifanyie hivi na hivi, tena aendelee hivyo, neno hilo, Adonia alilolisema, lisipokuwa la kuiangamiza roho yake! Sasa kwa hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, aliyenitia nguvu akinikalisha katika kiti cha kifalme cha baba yangu Dawidi, akanitengenezea nyumba, kama alivyosema, basi, kwa sababu hiyo Adonia sharti afe leo hivi! Mfalme Salomo akatuma kulitia jambo hilo mkononi mwake Benaya, mwana wa Yoyada, naye akampiga, hata akafa. Naye mtambikaji Abiatari mfalme akamwambia: Nenda Anatoti shambani kwako! Kwani wewe unapaswa na kufa; lakini leo hivi sitakuua, kwa kuwa ulilichukua Sanduku la Bwana Mungu mbele ya baba yangu Dawidi, tena ukateseka katika mateso yote yaliyompata baba yangu. Ndivyo, Salomo alivyomfukuza Abiatari, asiwe tena mtambikaji wa Bwana; akalitimiza lile neno la Bwana, alilolisema la mlango wa Eli kule Silo. Habari hizi zikamfikia Yoabu, maana Yoabu alikuwa ameandamana na Adonia, ingawa Abisalomu hakuandamana naye kumfuata; ndipo, Yoabu alipokimbilia Hemani mwa Bwana, akazishika pembe za meza ya Bwana. Mfalme Salomo akaambiwa: Yoabu amekimbilia Hemani mwa Bwana, yumo humo kandokando ya meza ya Bwana. Ndipo, Salomo alipomtuma Benaya, mwana wa Yoyada, akamwambia: Nenda, umpige! Benaya akaingia Hemani mwa Bwana, akamwambia: Hivi ndivyo, mfalme anavyosema: Toka! Akasema: Sitoki, kwani nitajifia hapa. Benaya akarudi kwake mfalme, akamwambia neno hilo la kwamba: Hivyo ndivyo, Yoabu alivyosema, ndivyo alivyonijibu. Mfalme akamwambia: Fanya, kama alivyosema, umpige hapo, kisha mzike! Ndivyo, utakavyoziondoa kwangu na kwa mlango wa baba yangu manza za zile damu, Yoabu alizozimwaga bure. Tena ndivyo, Bwana atakavyomrudishia zile damu zake kichwani pake, alizozimwaga na kupiga watu wawili waliokuwa waongofu na wema kuliko yeye akiwaua kwa upanga, baba yangu Dawidi asivijue, yule Abineri, mwana wa Neri, mkuu wa vikosi vya Isiraeli, na Amasa, mwana wa Yeteri, mkuu wa vikosi vya Yuda. Damu zao na zikirudie kichwa cha Yoabu na vichwa vya vizazi vyake kale na kale! Lakini kwake Dawidi na kwa vizazi vyake na kwa mlango wake na kwa kiti chake cha kifalme na kuweko kale na kale na matengemano yatokayo kwa Bwana! Ndipo, Benaya, mwana wa Yoyada, alipopanda, akampiga na kumwua, kisha akazikwa nyumbani mwake nyikani. Mfalme akamweka Benaya, mwana wa Yoyada, kuwa mkuu wa vikosi mahali pake, naye mtambikaji Sadoki mfalme akamweka kuwa mahali pa Abiatari. Kisha mfalme akatuma, akamwita Simei, akamwambia: Jijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae humo! Usitoke humo kwenda huko wala huko! Itakuwa hivi: siku, utakapotoka na kukivuka kijito cha Kidoroni, ujue kabisa, ya kuwa utakufa papo hapo, damu yako iwe kichwani pako. Simei akamwambia mfalme: Neno hili ni jema; kama bwana wangu mfalme alivyosema, ndivyo, mtumwa wako atakavyofanya. Kisha Simei akakaa Yerusalemu siku nyingi. Ikawa, miaka mitatu ilipopita, watumwa wawili wa Simei walimkimbilia Akisi, mwana wa Maka, mfalme wa Gati; watu wakamwambia Simei kwamba: Tazama, watumwa wako wako Gati. Ndipo, Simei alipomtandika punda wake, akaenda Gati kwa Akisi kuwatafuta watumwa wake; kisha Simei akaenda zake, akawaleta watumwa wake toka Gati. Salomo akaambiwa, ya kuwa Simei ametoka Yerusalemu kwenda Gati na kurudi. Ndipo, mfalme alipotuma kumwita Simei, akamwambia: Je? Sikukuapisha na kumtaja Bwana na kukushuhudia kwamba: Siku, utakapotoka na kwenda huko au huko, ujue kabisa, ya kuwa utakufa papo hapo? Nawe hukuniambia: Neno hili ni jema, nimesikia? Mbona hukukishika kiapo cha Bwana, wala agizo, nililokuagiza? Mfalme akamwambia Simei: Mwenyewe unayajua mabaya yote, moyo wako uliyoyawaza, uliyomtendea baba yangu Dawidi; sasa Bwana atayarudisha hayo mabaya yako kichwani pako. Lakini mfalme Salomo atakuwa amebarikiwa, nacho kiti cha kifalme cha Dawidi kitakuwa chenye nguvu mbele ya Bwana kale na kale. Kisha mfalme akamwagiza Benaya, mwana wa Yoyada, kwenda; naye akatoka, akampiga, hata akafa. Ndivyo, ufalme ulivyopata nguvu mkononi mwa Salomo. Salomo akaingia udugu na Farao, mfalme wa Misri, akimwoa binti Farao, akamwingiza mjini mwa Dawidi, mpaka akiisha kuijenga nyumba yake na Nyumba ya Bwana na boma la kuuzunguka Yerusalemu. Lakini watu walikuwa wakitambika vilimani, kwani Jina la Bwana halijajengewa nyumba bado mpaka siku hizo. Salomo akampenda Bwana, kwa hiyo akaendelea kuyafuata maongozi ya baba yake Dawidi, lakini naye alikuwa akitambika vilimani na kuvukizia huko. Mfalme akaenda Gibeoni kutambika huko, kwani hicho kilikuwa kilima kikuu cha kutambikia juu yake; Salomo akatoa ng'ombe elfu za tambiko za kuteketezwa nzima hapo pa kutambikia. Usiku huo Bwana akamtokea Salomo katika ndoto huko Gibeoni, Mungu akamwambia: Omba kwangu, uyatakayo, nikupe! Salomo akasema: Wewe ulimfanyizia mtumishi wako baba yangu Dawidi mambo ya upole mwingi, kwa kuwa alifanya machoni pako mwenendo wenye kweli na wongofu kwa moyo uliokunyokea; nawe hukuacha kumtolea huo upole mwingi, ukampa mwana anayekaa katika kiti chake cha kifalme, kama vilivyotokea leo hivi. Sasa Bwana Mungu wangu, wewe umempa mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa baba yangu Dawidi, nami nikingali mwana mdogo bado, sijui penye kutoka wala penye kuingia. Tena mtumishi wako yuko katikati yao walio ukoo wako, uliouchagua, nao ni watu wengi wasiowezekana wala kuhesabiwa wala kuwangwa kwa kuwa wengi. Kwa hiyo mpe mtumishi wako moyo wenye kutii, nipate kuwaamua walio ukoo wako na kuyatambua yaliyo mema nayo yaliyo mabaya! Kwani yuko nani anayeweza kuwaamua walio ukoo wako ulio wenye watu wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, kwa kuwa Salomo ameomba neno kama hilo. Ndipo, Mungu alipomwambia: Kwa kuwa umeomba neno kama hilo, ukaacha kuomba siku nyingi za kuwapo, wala hukujiombea mali nyingi, wala hukutaka kufa kwa adui zako, ukajiombea utambuzi wa kusikia mashauri, tazama, nimekwisha kufanya, kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wenye werevu wa kweli na utambuzi. Kwa hiyo mtu kama wewe hakuwako mbele yako, wala hataondokea nyuma yako atakayekuwa kama wewe. Nayo usiyoyaomba nimekupa, kama mali nyingi na utukufu; kwa hiyo mtu kama wewe hatakuwako katika wafalme siku zako zote za kuwapo. Kama utaendelea katika njia zangu na kuyaangalia maongozi yangu na maagizo yangu, kama baba yako Dawidi alivyoendelea, nitakupa hata siku nyingi za kuwapo. Salomo alipoamka akaona, ya kuwa ameota; alipofika Yerusalemu, akaja kusimama mbele ya Sanduku la Agano la Bwana, akatoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, akatengeneza nazo ng'ombe za tambiko za shukrani, akawafanyia watumishi wake wote karamu. Siku zile wakaja wanawake wagoni wawili kwa mfalme, wakasimama mbele yake. Mwanamke mmoja akamwambia: E bwana wangu, mimi na huyu mwanamke tunakaa katika nyumba moja, mimi nikazaa mtoto mle nyumbani, nilimo naye. Ikawa siku ya tatu ya kuzaa kwangu, huyu mwanamke akazaa naye, nasi tulikuwa pamoja mle nyumbani, hamna mgeni tena pamoja nasi, ni sisi wawili peke yetu mle nyumbani. Basi, usiku mtoto wake huyu mwanamke akafa, kwa kuwa alimlalia. Kisha akaamka usiku wa manane, akamchukua mtoto wangu kitandani kwangu, kijakazi wako alipolala usingizi, akamweka kifuani kwake, naye mtoto wake mfu akamweka kifuani kwangu. Asubuhi nilipoamka kumnyonyesha mtoto wangu, nikimtazama, amekufa. Kulipokucha vema, nikamchungulia sana, nimtambue, nikamwona, ya kuwa si mtoto wangu, niliyemzaa. Ndipo, yule mwanamke mwingine aliposema: Sivyo! Mtoto wangu ndiye aliye mzima, naye mtoto wako ndiye aliyekufa. Lakini yule akasema: Sivyo! Mtoto wako ndiye aliyekufa, naye mtoto wangu ndiye aliye mzima. Wakabishana hivyo mbele ya mfalme. Mfalme akasema: Huyu anasema: Mtoto huyu aliye mzima ni wangu, naye aliyekufa ni mtoto wako. Naye mwenziwe anasema: Sivyo! Mtoto wako ndiye aliyekufa, naye mtoto wangu ndiye aliye mzima. Kisha mfalme akasema: Nileteeni upanga! Walipoleta upanga mbele ya mfalme, mfalme akasema: Mkateni huyu mtoto mzima, atoke vipande viwili! Huyu mpeni kipande, naye mwingine kipande! Ndipo, yule mwanamke aliyekuwa mamake mtoto aliyeishi aliposema kwa kumwonea mtoto wake uchungu, akamwambia mfalme: E bwana wangu, mpeni mtoto mzima, msimwue kabisa! Lakini yule mwingine akasema: Asiwe wangu wala wako; haya! Mkateni! Ndipo, mfalme alipojibu akisema: Mpeni yule mtoto, akiwa mzima, msimwue kabisa! Yeye ni mama yake. Waisiraeli wote wakasikia, mfalme alivyolikata lile shauri, wakamwogopa mfalme, kwani wameona, ya kuwa moyoni mwake umo werevu wa Kimungu wa kuwaamulia watu. Mfalme Salomo akawa mfalme wa Waisiraeli wote; nao hawa walikuwa wakuu wake: Azaria, mwana wa Sadoki, alikuwa mtambikaji. Elihorefu na Ahia, wana wa Sisa, walikuwa waandishi; Yosafati, mwana wa Ahiludi, alikuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa. Benaya, mwana wa Yoyada, alikuwa mkuu wa vikosi, Sadoki na Abiatari walikuwa watambikaji. Azaria, mwana wa Natani, alikuwa mkuu wa waangaliaji, naye mtambikaji Zabudi, mwana wa Natani, alikuwa mpenzi wa mfalme. Ahisari alikuwa mkuu wa nyumbani, naye Adoniramu, mwana wa Abuda, alikuwa mkuu wa kazi za nguvu. Salomo alikuwa na waangaliaji kumi na wawili waliowekwa kuwaangalia Waisiraeli wote, ndio waliompatia mfalme nao wa nyumbani mwake vyakula, ikawa kila mmoja akaleta vyakula vya mwezi mmoja katika mwaka. Nayo majina yao ni haya: Mwana wa Huri milimani kwa Efuraimu; mwana wa Dekeri alikuwako Makasi na Salabimu na Beti-Semesi na Eloni na Beti-Hanani. Mwana wa Hesedi huko Aruboti, hata Soko na nchi yote ya Heferi ilikuwa yake. Mwana wa Abinadabu vilima vyote vya Dori vilikuwa vyake, naye Tafati binti Salomo alikuwa mkewe. Baana, mwana wa Ahiludi, yake ilikuwa Taanaki na Megido na Beti-Seani yote iliyoko kandokando ya Sartani chini ya Izireeli toka Beti-Seani hata Abeli-Mehola mpaka ng'ambo ya pili ya Yokimamu. Mwana wa Geberi alikuwako vilimani kwa Gileadi; navyo vijiji vya Yairi, mwana wa Manase, vilivyoko Gileadi vilikuwa vyake, hata nchi ya Argobu iliyoko Basani, ni miji mikubwa 60 yenye maboma na makomeo ya shaba. Ahinadabu, mwana wa Ido, alielekea Mahanaimu. Ahimasi alikuwako Nafutali, naye alimchukua Basimati, binti Salomo, awe mkewe. Baana, mwana wa Husai, alikuwako Aseri na Baloti. Yosafati, mwana wa Parua, alikuwako Isakari. Simei, mwana wa Ela, alikuwako Benyamini. Geberi, mwana wa Uri, alikuwako katika nchi ya Gileadi iliyokuwa nchi ya Sihoni, mfalme wa Waamori, na ya Ogi, mfalme wa Basani. Naye mwangaliaji aliyewekwa katika nchi hizi alikuwa yeye mmoja. Nao Wayuda na Waisiraeli walikuwa wengi, kama mchanga ulioko ufukoni kwenye bahari ulivyo mwingi; walikuwa wakila, wakinywa na kufurahi. Salomo akawa akizitawala nchi za kifalme zote kutoka lile jito kubwa kuifikia nchi ya Wafilisti hata mipaka ya Misri; walimletea mahongo, wakamtumikia Salomo siku zake zote za kuwapo. Vyakula, Salomo alivyovitumia kwa siku moja, vilikuwa kori 30, ndio frasila 300 za unga mzuri na kori 60, ndio frasila 600 za unga mwingine; tena ng'ombe 10 waliononeshwa na ng'ombe 20 wa malishoni na kondoo 100, tena kulungu na paa na funo na mabata waliononeshwa hawakuhesabiwa. Kwani alikuwa akizitawala nchi zote za ng'ambo ya huku ya lile jito kutoka Tifusa hata Gaza, nao wafalme wote wa ng'ambo ya huku ya lile jito aliwatawala, kukawa na utengemano katika nchi zake zote zilizomzunguka. Wayuda na Waisiraeli wakakaa na kutulia kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mkuyu wake kutoka Dani kufikia Beri-Seba siku zote, Salomo alizokuwapo. Salomo alikuwa na majozi ya farasi 40000 ya magari yake, tena wapanda farasi 12000. Nao wale waangaliaji wakampatia mfalme Salomo vyakula nao wote walioikaribia meza ya mfalme Salomo, kila mmoja wao mwezi wake, hawakuwakosesha kitu cho chote. Nao mtama na mabua ya ngano ya farasi wa kupanda na wa magari wakayapeleka mahali hapo, alipokuwa, kila mtu hapo, alipoagizwa. Mungu akampa Salomo werevu wa kweli na utambuzi mwingi sana na akili za moyo zilizokuwa nyingi kama mchanga ulioko ufukoni kwenye bahari. Werevu wa kweli wa Salomo ukazidi kuliko werevu wao wote waliokuwa werevuwa kweli upande wa maawioni kwa jua, nao warevu wote wa kweli ulioko Misri. Akawa mwerevu wa kweli kuliko watu wote pia, akamshinda naye Etani wa Ezera na Hemani, hata Kalkoli na Darda, wana wa Maholi; jina lake likasifiwa katika mataifa yote pande zote. Akasema mifano 3000, nazo nyimbo zake zikawa 1005. Akaiimbia miti kuanzia miangati iliyoko Libanoni kufikisha hata mivumbasi imeayo mahameni, akawaimbia nao nyama wa porini na ndege na wadudu na samaki. Watu wakaja na kutoka katika makabila yote, wausikilize werevu wa kweli wa Salomo, wakatoka hata kwa wafalme wote wa huku nchini waliopata habari ya werevu wake wa kweli. Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma watumishi wake kwa Salomo, kwani alisikia, ya kuwa wamempaka mafuta, awe mfalme mahali pa baba yake, kwani Hiramu alikuwa akimpenda Dawidi siku zote. Salomo akatuma kwa Hiramu kumwambia: Wewe unajua, ya kuwa baba yangu Dawidi hakuweza kulijengea Jina la Bwana Mungu wake nyumba kwa ajili ya vita, adui zake walivyomletea toka pande zote, hata Bwana akawaweka chini ya nyayo za miguu yake. Sasa Bwana Mungu wangu amenipa kutulia pande zote, hakuna mpingani wala jambo baya. Kwa hiyo nimesema, nilijengee Jina la Bwana Mungu wangu nyumba, kama Bwana alivyomwambia baba yangu Dawidi kwamba: Mwanao, nitakayempa kukaa mahali pako katika kiti chako cha kifalme, ndiye atakayelijengea Jina langu nyumba. Sasa agiza, watu wanikatie miangati huko Libanoni! Watu wangu na wachanganyike na watu wako, nao mshahara wote wa watu wako nitakupa, kama utakavyosema, kwani mwenyewe unajua, ya kuwa kwetu hakuna ajuaye kuchonga miti kama watu wa Sidoni. Ikawa, Hiramu alipoyasikia haya maneno ya Salomo akafurahi sana, akasema: Bwana na atukuzwe leo hivi, kwani amempa Dawidi mwana mwenye werevu wa kweli wa kuwatawala wale watu wengi. Ndipo, Hiramu alipotuma kwa Salomo kumwambia: Nimeyasikia maneno yako, uliyotuma kuniambia. Mimi nitayafanya yote, uyatakayo, nikupatie miti ya miangati na miti ya mivinje. Watu wangu wataitelemsha toka Libanoni hata baharini; kisha mle baharini nitaifunga, ielee; ndivyo, nitakavyoifikisha mahali pale, utakaponiambia; hapo nitaifungua tena, wewe upate kuichukua. Nawe na uyafanye, niyatakayo, ukiwapa watu wa kwangu vyakula. Kisha Hiramu akampa Salomo miti ya miangati na miti ya mivinje, yote kama alivyoitaka. Naye Salomo akampa Hiramu kori 20000, ndio frasila 200000 za ngano kuwa posho za watu wa kwake na kori 20, ndio frasila 200 za mafuta mazuri mno; hivi ndivyo, Salomo alivyompa Hiramu mwaka kwa mwaka. Bwana akampa Salomo werevu wa kweli, kama alivyomwambia. Kwao Hiramu na Salomo yakawako matengemano, wakafanya agano hao wawili. Kisha mfalme Salomo akawatoza Waisiraeli wote watu wa kazi za nguvu, nao hao watu wa kazi za nguvu wakawa watu 30000. Akatuma kila mwezi watu 10000 kwenda Libanoni, wapokeane hivyo: mwezi mmoja wakae Libanoni, kisha nyumbani kwao miezi miwili. Naye Adoniramu alikuwa mkuu wao hao watu wa kazi za nguvu. Salomo akawa nao wachukuzi wa mizigo 70000, tena wachonga mawe 80000 milimani. Tena Salomo akawa na wasimamizi 3300 waliowekwa naye kuwa wakuu wa wafanya kazi na kuwasimamia, wakifanya kazi. Mfalme akaagiza, wavunje mawe yaliyo makubwa na mazuri mno ya kuchonga ya kuwekea misingi ya nyumba. Waashi wa Salomo na waashi wa Hiramu na Wagebali wakayachonga. Ndivyo, walivyotengeneza miti na mawe, wapate kuijenga hiyo nyumba. Ikawa katika mwaka wa 480, tangu wana wa Isiraeli walipotoka Misri, katika mwaka wa nne, Salomo alipokuwa mfalme wa Waisiraeli, katika mwezi wa Ziwu, ndio mwezi wa pili, ndipo, alipomjengea Bwana nyumba. Nayo hiyo nyumba, mfalme Salomo aliyomjengea Bwana, urefu wake wa kwenda mbele ulikuwa mikono 60, nao upana wake mikono 20, nao urefu wake wa kwenda juu mikono 30. Nao ukumbi uliokuwa usoni pake jumba hilo takatifu urefu wake wa kwenda mbele ulikuwa mikono 20, upatane na upana wa nyumba yenyewe, upana wake ulikuwa mikono kumi kuufuata urefu wa nyumba wa kwenda mbele. Akaitia hiyo nyumba madirisha yenye miti iliyoungwa. Tena kando ya ukuta wa nyumba kuizunguka yote akajenga vyumba vilivyozizunguka kuta za nyumba pande zote za hapo Patakatifu napo hapo penye chumba cha nyuma; hivyo vyumba akavitengeneza ubavuni pande zote. Navyo hivyo vyumba vya chini upana wao ulikuwa mikono mitano, navyo vya katikati upana wao mikono sita, navyo vya juu upana wao mikono saba. Kwani nje kuta zilipunguka kuwa zenye vipago kuizunguka nyumba yote, kusudi boriti zao hivyo vyumba visishikamane na nyumba yenyewe mle kutani ndani. Hapo, nyumba ilipojengwa, ikajengwa kwa mawe yaliyokwisha kuchongwa yalipovunjwa; mahali hapo, nyumba ilipojengwa, hapakusikilika nyundo wala shoka wala chombo cho chote cha chuma. Mlango wa vyumba vya ubavuni ulikuwa katikati upande wa kulia wa nyumba; wakapanda kwa ngazi iliyojipinda kufikia vyumba vya katikati, vivyo hivyo kuvitoka vyumba vya katikati kuvifikia vile vya juu. Alipokwisha kuijenga hiyo nyumba akaipamba na kutumia boriti na mbao za miangati. Navyo vile vyumba vya ubavuni vya nyumba yote nzima akavijenga kuwa vyenye urefu wa kwenda juu mikono mitano, navyo vikashikamana na nyumba yenyewe kwa boriti za miangati. Neno la Bwana likamjia Salomo la kwamba: Kwa hivyo, unavyoijenga nyumba hii, utakapoendelea katika maongozi yangu na kuyafanya maamuzi yangu na kuyaangalia maagizo yangu yote, uyafuate, ndipo, nitakapolitimiza kwako neno langu, nililomwambia baba yako Dawidi: Nitakaa katikati yao wana wa Isiraeli, nisiwaache walio ukoo wangu wa Waisiraeli. Salomo alipokwisha kuijenga hiyo nyumba na kuimaliza, akazitia kuta za hiyo nyumba upande wa nyumbani mbao za miangati; kuanzia chini penye msingi wa nyumba mpaka juu penye boriti, akazifunika kuta za nyumbani kwa mbao, hata chini nyumbani pa kukanyagia akapafunika kwa mbao za mivinje. Kisha akajenga chumba mle nyumbani upande wa nyuma urefu wa mikono 20 kwa mbao za miangati kuanzia chini mpaka juu ukutani; ndivyo, alivyojenga mle nyumbani chumba cha nyuma kuwa Patakatifu Penyewe. Lakini chumba kilichokuwa mbele yake kilikuwa cha mikono 40, nacho ndicho chumba cha Patakatifu. Hivyo upande wa ndani wa hiyo nyumba ulikuwa miangati tu yenye urembo wa mifano ya matango na ya maua yachanukayo; po pote ni miangati, mawe hayakuonekana. Nacho chumba cha nyuma mle ndani nyumbani alikitengeneza cha kuwekea humo Sanduku la Agano la Bwana. Hicho chumba cha nyuma urefu wake wa kwenda mbele ulikuwa mikono 20, nao upana wake mikono 20, nao urefu wake wa kwenda juu mikono 20, akakifunikiza chote dhahabu zilizong'azwa. Nayo meza ya kutambikia akaifunikiza kwa mbao za miangati. Upande wa ndani wa hiyo nyumba Salomo akaufunikiza dhahabu zilizong'azwa, akapitisha mbele ya chumba cha nyuma minyororo ya dhahabu, nacho akakifunikiza dhahabu. Hivyo nyumba yote akaifunikiza dhahabu, akaimaliza nyumba yote nzima hivyo, nayo meza ya kutambikia iliyokuwa mbele ya chumba cha nyuma akaifunikiza dhahabu. Mle ndani ya chumba cha nyuma akatengeneza Makerubi mawili ya miti ya michekele, urefu wao wa kwenda juu ulikuwa mikono kumi. Kila bawa moja la Kerubi lilikuwa mikono mitano, nalo bawa la pili la Kerubi lilikuwa mikono mitano, ikawa mikono kumi kutoka pembe ya bawa lake moja mpaka pembe ya bawa lake jingine. Vilevile Kerubi la pili lilikuwa lenye mikono kumi; Makerubi yote mawili yalikuwa yenye kipimo kimoja na yenye sura moja. Urefu wa kwenda juu wa Kerubi moja ulikuwa mikono kumi, nalo Kerubi la pili lilikuwa vivyo hivyo. Akayaweka haya Makerubi katikati ya chumba cha ndani, yakiwa yameyakunjua mabawa yao, bawa la moja liligusa ukuta, nalo bawa lake lile la pili liligusa ukuta wa pili, nayo mabawa yao yaliyoelekea upande wa nyumbani kati yaligusana bawa kwa bawa. Haya Makerubi akayafunikiza dhahabu. Namo katika kuta zote za nyumbani katika chumba cha ndani na cha nje akachora machoro ya mifano ya Makerubi na ya mitende na ya maua yachanukayo. Napo pa kukanyagia nyumbani chini akapafunikiza dhahabu katika chumba cha ndani na cha nje. Tena pa kukiingilia chumba cha ndani akatengeneza lango lenye milango miwili ya mbao za michekele, vizingiti na miimo ilikuwa yenye miraba mitano. Namo katika hiyo milango miwili ya mbao za michekele akachora machoro ya Makerubi na ya mitende na ya maua yachanukayo, kisha akaifunikiza dhahabu; hizo dhahabu za kuyafunikiza Makerubi na mitende zilikuwa zimesanwa. Vivyo hivyo hata penye kukiingilia chumba kitakatifu akatengeneza miimo ya miti ya michekele yenye miraba minne, na milango miwili ya mbao za mivinje, mlango mmoja ukipata kugeuka pande mbili, nao mlango wa pili uligeuka pande mbili. Akachora namo humo Makerubi na mitende na maua yachanukayo, akaifunikiza dhahabu zilizopatanishwa kuwa sawa na yale machoro. Kisha akaujengea ua wa ndani ukuta wenye safu tatu za mawe ya kuchonga na safu moja ya boriti za miangati. Katika mwaka wa nne msingi wa nyumba ya Bwana uliwekwa katika mwezi wa Ziwu. Katika mwaka wa kumi na moja katika mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, nyumba ikamalizika pande zake zote, kama ilivyopasa; basi, ilikuwa miaka saba, aliyoijenga. Nyumba yake Salomo akaijenga miaka kumi na mitatu, mpaka akaimaliza hiyo nyumba yake yote. Kwanza akaijenga nyumba ya mwituni kwa Libanoni, urefu wake wa kwenda mbele ulikuwa mikono mia nao upana wake mikono hamsini nao urefu wake wa kwenda juu mikono thelathini; ilikuwa juu ya safu nne za nguzo za miangati, nazo boriti za miangati zilikuwa zimewekwa juu ya hizo nguzo. Vyumba vyake vilikuwa juu ya hizo nguzo, vikafunikwa juu penye dari kwa mbao za miangati, navyo vilikuwa arobaini na vitano, kila safu kumi na vitano. Nayo miamba ilikuwako safu tatu, hata madirisha yaliyoelekeana dirisha kwa dirisha, hivyo mara tatu. Milango yote na miimo yote ilikuwa ya nguzo zenye miraba, hata madirisha yaliyoelekeana dirisha kwa dirisha, hivyo mara tatu. Kisha akatengeneza ukumbi wenye nguzo, urefu wake wa kwenda mbele ulikuwa mikono hamsini, upana wake mikono thelathini; mbele yake kulikuwa na ukumbi mwingine wenye nguzo na kipago mbele yao. Kisha akatengeneza ukumbi wa kiti cha kifalme kuwa baraza ya shauri, atakamokatia mashauri ya watu; ukafunikwa mbao za miangati toka chini hata juu. Kisha akaijenga nyumba yake ya kukaa humo katika ua wa pili upande wa ndani wa ukumbi huo, nayo ikajengwa vivyo hivyo. Tena akajenga nyumba ya binti Farao, Salomo aliyemwoa, ikawa vivyo hivyo kama ule ukumbi. Majengo haya yote yalikuwa yamejengwa kwa mawe mazuri yaliyochongwa kwa kipimo na kukatwa kwa misumeno upande wa nyumbani na wa nje, kutoka kwenye msingi mpaka juu kwenye mawe yanayotokea kidogo toka nje kufikia ua mkubwa. Nayo misingi ilikuwa imewekewa mawe mazuri makubwa mno, mengine ya mikono kumi, mengine ya mikono minane. Juu yao palikuwa na mawe mazuri yaliyochongwa kwa kipimo, tena miangati. Ua mkubwa ukazunguka po pote wenye ukuta wa safu tatu za mawe ya kuchonga na safu moja ya boriti za miangati. Ndivyo, vilivyokuwa hata penye ua wa ndani wa nyumba ya Bwana na penye ua wa ukumbi wa nyumba yake. Kisha mfalme Salomo akatuma kumchukua Hiramu kule Tiro: alikuwa mwana wa mwanamke mjane wa shina la Nafutali, naye baba yake alikuwa mtu wa Tiro aliyefua shaba. Huyu alikuwa mwenye werevu wa kweli na utambuzi na ujuzi wote wa kuzitengeneza kazi zote pia kwa shaba. Huyu akaja kwa mfalme Salomo, akamfanyizia hizo kazi zote. Akatengeneza nguzo mbili za shaba, urefu wake nguzo moja ulikuwa mikono kumi na minane, tena uzi wa mikono kumi na miwili ukaizunguka, nayo nguzo ya pili ilikuwa hivyo. Akafanya hata vichwa viwili vya kuviweka juu ya hizi nguzo, vilitengenezwa kwa shaba iliyoyeyushwa; kichwa kimoja urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono mitano, nao wake wa pili mikono mitano. Tena misuko iliyotengenezwa kwa nyuzi zilizokuwa kama mikufu ikavifunika vichwa vilivyokuwa juu ya nguzo, kichwa kimoja kikapata saba, nacho cha pili saba. Kisha akatengeneza komamanga, mistari miwili ya kuzunguka penye msuko mmoja uliokuwa wa kuvifunika vichwa vilivyokuwa juu ya hizo nguzo, nao wa pili akautengeneza vivyo hivyo. Navyo hivyo vichwa vilivyokuwa juu ya nguzo penye ukumbi vilikuwa vimetengenezwa kuwa kama maua ya uwago yenye mikono minne. Hivyo vichwa vya juu ya hizo nguzo vilikuwa juu penye ukingo uliokuwa wenye ile misuko. Nazo komamanga zilikuwa 200, zikauzunguka nao msuko wa nguzo ya pili kwa mistari-mistari. Kisha akazisimamisha hizo nguzo penye ukumbi wa jumba hili; alipoisimamisha nguzo ya kuumeni akaiita jina lake Yakini (Hushikiza); tena alipoisimamisha nguzo ya kushotoni akaiita jina lake Boazi (Nguvu imo). Tena vichwa vya hizo nguzo vilikuwa vimetengenezwa kuwa kama maua ya uwago. Ndivyo, kazi za hizo nguzo zilivyomalizika. Kisha akaitengeneza ile bahari kwa shaba iliyoyeyushwa; toka ukingo wake wa huku hata ukingo wa huko ilikuwa mikono kumi; iliviringana pande zote, urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono mitano, nayo kamba ya kuizunguka pande zote ilikuwa ya mikono thelathini. Chini ya ukingo wake kuizunguka pande zote palikuwa na mifano ya matango, kumi kwa mkono mmoja, ikaizunguka hiyo bahari pande zote, hiyo mifano ya matango ilikuwa mistari miwili, nayo ilikuwa imeyeyushiwa mumo, bahari ilipoyeyushwa. Ikakaa juu ya ng'ombe kumi na mbili, tatu zilielekea kaskazini, tatu zilielekea baharini, tatu zilielekea kusini, tatu zilielekea maawioni kwa jua, nayo bahari ilikuwa juu yao, nayo mapaja yao yote yalikuwa yameelekea ndani. Unene wake ulikuwa upana wa shibiri, nao ukingo wake wa juu ulikuwa kama wa kikombe au kama wa ua la uwago. Ndani yake zilienea bati 2000, ndip pishi 18000. Kisha akatengeneza vilingo kumi vya shaba. Urefu wa kwenda mbele wa kila kilingo kimoja kilikuwa mikono minane nao upana wake ulikuwa mikono minne, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono mitatu. Hivi vilingo vilikuwa vimetengenezwa hivyo: vilikuwa na vibao vya kufungia, hivi vibao vilikuwa katikati ya vilingo. Namo katika hivi vibao vilivyokuwa katikati ya vilingo mlikuwa na simba na ng'ombe na Makerubi, vilevile katika vilingo juu na chini ya hizo simba na ng'ombe palikuwa pametengenezwa kata za maua zilizoning'inia. Kila kilingo kimoja kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, navyo vyuma vya kuyashikia vilikuwa vya shaba; tena miguu yao minne ilikuwa yenye vishikio, navyo hivi vishikio vilikuwa vimetiwa kwa kuyeyushwa chini ya bakuli, tena kando yao kila mmoja pametiwa kata zilizoelekeana. Kinywa chake kilikuwa ndani ya kilemba, kikatokea juu kipande cha mkono; hicho kinywa chake kikaviringana, maana kilitengenezwa kuwa hivyo, upana wake ukawa mkono mmoja na nusu. Napo penye kinywa chake palikuwa na machoro; lakini vile vibao vya kufungia vilikuwa vyenye miraba, havikuviringana. Yale magurudumu manne yalikuwa chini ya vibao vya kufungia, navyo vyuma vya kuyashikia magurudumu vilikuwa vimeungwa na kilingo, nao urefu wa kwenda juu wa gurudumu moja ulikuwa mkono mmoja na nusu. Hayo magurudumu yalikuwa yametengenezwa kama magurudumu ya magari, lakini vyuma vyao vya kuyashikia na miviringo yao ya nje na vijiti vyao na vichwa vyao vya kati vyote pia vilikuwa vya shaba iliyoyeyushwa. Penye pembe zote nne za kila kilingo palikuwa na vishikio vinne; hivi vishikio vilikuwa vimeunganika na kilingo chao chenyewe. Juu ya kilingo palikuwa kama kilingo kidogo kilichoviringana pande zote, urefu wa kwenda juu ulikuwa nusu ya mkono tu; hapo juu ya kilingo palikuwa navyo vyuma vya kushikia bakuli na vibao vyake vya kufungia, vyote vilikuwa vimeunganika nacho. Katika mabamba ya vyuma vyake vya kushikia na katika vibao vyake vya kufungia akachora Makerubi na simba na mitende, po pote kama palivyokuwa na nafasi, kisha akachora kata za maua za kuyazungusha yale machoro. Hivyo ndivyo, alivyovitengeneza vile vilingo kumi, vyote pia viliyeyushwa kwa njia moja, nacho kipimo chao kilikuwa kimoja, nao mfano wao ulikuwa mmoja. Kisha akatengeneza mitungi kumi ya shaba, katika mtungi mmoja zilienea bati 40, ndio pishi 360, nao upana wa kila mtungi mmoja ulikuwa mikono minne, akaweka katika vilingo vile kumi mtungi mmoja katika kila kilingo kimoja. Akaweka vilingo vitano kuumeni kwa ile nyumba na vitano kushotoni kwake ile nyumba, nayo ile bahari akaiweka kuumeni kwa ile nyumba kunakoelekea maawioni kwa jua, lakini kusini kidogo. Kisha Hiramu akatengeneza mitungi na majembe na vyano. Hiramu akazimaliza kazi zote, alizomfanyizia mfalme Salomo nyumbani mwa Bwana: nguzo mbili zenye vilemba vya vile vichwa viwili vilivyoko juu ya hizo nguzo na misuko miwili kama ya mkeka ya kuvifunika vile vilemba viwili vya vichwa vilivyoko juu ya hizo nguzo; tena komamanga 400 zilizotiwa katika ile misuko, kila msuko mmoja ukipata mistari miwili ya komamanga ya kuvifunika vile vilemba viwili vya vichwa vilivyoko juu ya hizo nguzo; tena vile vilingo kumi na mitungi kumi iliyowekwa juu ya hivyo vilingo; tena ile bahari moja na zile ng'ombe kumi na mbili zilizokuwa chini ya ile bahari; nayo masufuria na majembe na vyano. Vyombo hivi vyote, Hiramu alivyomtengenezea mfalme Salomo, avitie nyumbani mwa Bwana, vilikuwa vya shaba iliyong'aa. Naye mfalme alikuwa ameagiza kuviyeyusha katika bwawa la Yordani penye udongo mgumu katikati ya miji ya Sukoti na Sartani. Salomo akaviweka tu vyombo hivi vyote; kwa kuwa vingi sanasana shaba zilizotumiwa hazikupimwa, wala hazikuulizwa, kama ni ngapi. Ndivyo, Salomo alivyovitengeneza vyombo vyote vya kutumiwa nyumbani mwa Bwana. Lakini meza ya kutambikia ilikuwa ya dhahabu, nayo meza ya kumwekea Bwana mikate ilikuwa ya dhahabu; navyo vile vinara, vitano vya kuviweka kuumeni, na vitano vya kuviweka kushotoni mbele ya Patakatifu Penyewe, vilikuwa vya dhahabu zilizong'azwa, nayo maua na taa na koleo zao zilikuwa za dhahabu; tena mabakuli na makato ya kusafishia mishumaa na vyano na kata na sinia zilikuwa za dhahabu zilizong'azwa. Nazo bawaba za milango ya chumba cha ndani pa kupaingilia Patakatifu Penyewe nazo za milango ya chumba kikubwa cha Patakatifu zilikuwa za dhahabu. Kazi zote, ambazo mfalme Salomo aliifanyia nyumba ya Bwana, zilipomalizika, Salomo akavipeleka vipaji vitakatifu vyote vya baba yake Dawidi, zile fedha na dhahabu na vile vyombo, akaviweka penye vilimbiko vya nyumba ya Bwana. Kisha Salomo akawakusanya wazee wa Waisiraeli nao wote waliokuwa vichwa vya mashina na wakuu wa milango ya wana wa Isiraeli mle Yerusalemu kwake yeye mfalme Salomo kwenda kulitoa Sanduku la Agano la Bwana katika mji wa Dawidi ulioitwa Sioni. Ndipo, watu wote wa Isiraeli walipokusanyika kwa mfalme Salomo kufanya sikukuu katika mwezi wa Etanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Isiraeli walipokwisha fika, watambikaji wakalichukua hilo Sanduku. Wakalipeleka Sanduku la Bwana pamoja na Hema la Mkutano na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa Hemani; hivi watambikaji na Walawi wakavipandisha. Naye mfalme Salomo pamoja na mkutano wote wa Waisiraeli wote waliokusanyika kwake kuwa naye mbele ya hilo Sanduku wakatoa mbuzi na kondoo na ng'ombe kuwa ng'ombe za tambiko, nao hawakuhesabika, wala hawakuwangika kwa kuwa wengi mno. Watambikaji wakaliingiza Sanduku la Agano la Bwana mahali pake katika chumba cha ndani kiitwacho Patakatifu Penyewe, wakaliweka chini ya mabawa ya Makerubi. Kwani yale Makerubi yalikuwa yameyakunjua mabawa juu ya mahali pale, Sanduku lilipowekwa; ndivyo, Makerubi yalivyolifunika juu hilo Sanduku nayo mipiko yake. Kwa urefu wa mipiko pembe zao hii mipiko zikaonekana mle Patakatifu kuelekea mle chumbani mwa ndani, lakini nje hazikuonekana; nayo imo humo hata siku hii ya leo. Mle Sandukuni hamkuwamo na kitu, ni zile mbao mbili za mawe tu, Mose alizoziweka humo huko Horebu, Bwana alipofanya Agano na wana wa Isiraeli, walipotoka katika nchi ya Misri. Ikawa, watambikaji walipotoka Patakatifu, ndipo, wingu lilipoijaza Nyumba ya Bwana. Nao watambikaji hawakuweza kusimama humo na kuzifanya kazi za utumishi wao kwa ajili ya hilo wingu, kwani utukufu wa Bwana uliijaza Nyumba ya Bwana. Ndipo, Salomo aliposema: Bwana alisema, ya kuwa hukaa mawinguni mwenye weusi. Nami nimekujengea Nyumba, iwe Kao lako la kukaa humu kale na kale. Kisha mfalme akaugeuza uso wake, akaubariki mkutano wote wa Waisiraeli, nao wote wa mkutano wa Waisiraeli walikuwa wamesimama. Akasema: Atukuzwe Bwana Mungu wa Isiraeli! Aliyomwambia baba yangu Dawidi kwa kinywa chake, ameyatimiza kwa mkono wake, ya kwamba: Tangu siku ile, nilipoutoa ukoo wangu wa Waisiraeli huko Misri, sikuchagua mji katika mashina yote ya Isiraeli, ndimo wanijengee Nyumba, Jina langu likae humo. Lakini nilimchagua Dawidi wa kuutawala ukoo wangu wa Waisiraeli. Baba yangu Dawidi akawaza moyoni kulijengea Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli nyumba. Lakini Bwana akamwambia baba yangu Dawidi: Ukiwaza moyoni mwako kulijengea Jina langu nyumba, umefanya vema kuyawaza hayo moyoni mwako. Lakini wewe hutaijenga hiyo nyumba, ila mwanao atakeyetoka viunoni mwako ndiye atakayelijengea Jina langu nyumba. Bwana akalitimiza hilo neno, alilolisema, nami nikaondokea mahali pa baba yangu Dawidi, nikakaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli, kama Bwana alivyosema, nikalijengea Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli Nyumba hii. Nikapata humu mahali pa kuliwekea Sanduku, Agano la Bwana lilimo, alilolifanya na baba zetu alipowatoa katika nchi ya Misri. Kisha Salomo akaja kusimama mbele ya meza ya kumtambikia Bwana machoni pao mkutano wote wa Waisiraeli, akaikunjua mikono yake na kuielekeza mbinguni, akasema: Bwana Mungu wa Isiraeli, hakuna Mungu afananaye na wewe, wala mbinguni juu wala katika nchi huku chini. Unawashikia watumishi wako agano lako na upole wako, wakiendelea mbele yako kwa mioyo yao yote. Umemshikia mtumishi wako, baba yangu Dawidi, uliyomwambia; uliyoyasema kwa kinywa chako, umeyatimiza kwa mkono wako, kama inavyoonekana siku hii ya leo. Na sasa Bwana Mungu wa Isiraeli, mshikie mtumishi wako, baba yangu Dawidi, uliyomwambia kwamba: Kwako hakutakoseka mtu atakayekaa machoni pangu katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli, wanao wakiziangalia tu njia zao, waendelee kuwa machoni pangu, kama wewe ulivyoendelea kuwa machoni pangu. Sasa Mungu wa Isiraeli, hilo neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, baba yangu Dawidi, na lishupazwe! Inakuwaje? Mungu anakaa kweli huku nchini? Tazama! Mbingu nazo mbingu zilizoko juu ya mbingu hazikuenei, sembuse Nyumba hii, niliyoijenga! Yageukie maombo ya mtumishi wako na malalamiko yake, Bwana Mungu wangu, uvisikilize vilio na maombo, mtumishi wako anayokuomba usoni pako leo hivi! Uwe macho kuiangalia Nyumba hii usiku na mchana, ipate kuwa mahali pale, ulipopasema: Mahali hapa ndipo, Jina langu litakapokuwa! Kwa hiyo yasikie maombo, mtumishi wako atakayokuomba mahali hapa! Yasikie nayo malalamiko ya mtumishi wako nayo yao walio ukoo wako wa Waisiraeli, watakayokuomba mahali hapa! Wewe wasikie huko juu mbinguni, unakokaa! Tena utakapowasikia uwaondolee makosa! Mtu akikosana na mwenziwe, akachukuliwa, aape, basi, wakimwapisha hivyo, naye akija kuapia mbele ya meza ya kutambikia katika Nyumba hii, wewe umsikie huko mbinguni, ulitengeneze jambo hilo na kuwaamua watumishi wako, ukimlipisha yule aliyekosa na kumtwika kichwani pake matendo yake, tena yule asiyekosa ukimtokeza kuwa pasipo kosa, ukimpa yaliyo haki yake. Itakuwa, walio ukoo wako wa Waisiraeli wakimbizwe na adui, kwa kuwa wamekukosea; kisha watakapokurudia na kuliungama Jina lako, wakuombe na kukulalamikia humu Nyumbani, wewe na uwasikie huko mbinguni, uwaondolee walio ukoo wako wa Waisiraeli makosa yao! Kisha warudishe katika nchi hii, uliyowapa baba zao! Itakuwa, mbingu zizibane, mvua isinye, kwa kuwa wamekukosea; kisha watakapoombea mahali hapa na kuliungama Jina lako na kuyaacha makosa yao, kwa kuwa umewatea, wewe na uwasikie huko mbinguni, uwaondolee makosa yao walio watumishi wako nayo yao walio ukoo wako wa Waisiraeli! Kisha wafundishe njia iliyo njema, waishike, upate kuinyeshea nchi yako mvua tena, kwa kuwa umeipa walio ukoo wako, iwe fungu lao. Itakuwa, njaa iingie katika nchi hii au magonjwa mabaya, itakuwa, jua kali linyaushe mashamba yote, itakuwa, nzige na funutu wamalize vilaji vyote, itakuwa, adui zao wawasonge watu kwao malangoni mwao, itakuwa, mapigo menginemengine na magonjwa yo yote yawapate, basi, lisikie kila ombo na kila lalamiko litakalokutokea, kama ni la mtu mmoja awaye yote, au lao wote walio ukoo wako wa Waisiraeli, kwa kuwa kila mtu anayajua mapigo ya moyo wake. Hapo watakapokuja kuikunjua mikono yau humu Nyumbani, wewe na uwasikie huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa, uwaondolee makosa ukifanya yapasayo na kumrudishia kila mtu, kama njia zake zilivyo, kwa hivyo, unavyoujua moyo wake! Kwani wewe peke yako unaijua mioyo ya wana wa watu wote, kusudi wakuogope siku zote, watakazokuwapo katika nchi hii, uliyowapa baba zetu. Tena itakuwa, hata mgeni asiye wa ukoo wako wa Waisiraeli aje huku na kutoka katika nchi ya mbali kwa ajili ya Jina lako, kwani watapata habari za Jina lako lililo kuu na za kiganja chako kilicho na nguvu na za mkono wako uliokunjuka; basi, hapo atakapokuja, aombee humu Nyumbani, wewe na umsikie huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa, uyafanye yote, yule mgeni atakayokuomba na kukulilia, makabila yote ya nchi yalijue Jina lako, wakuogope kama wao walio ukoo wako wa Waisiraeli, tena wajue, ya kuwa Nyumba hii, niliyoijenga, imeitwa kwa Jina lako. Itakuwa, walio ukoo wako wakitoka kupigana na adui zao na kuishika njia, utakayowatuma, wakuombe, Bwana, njiani na kuuelekea mji huu, uliouchagua, hata Nyumba hii, niliyolijengea Jina lako, basi, hapo na uyasikie huko mbinguni maombo yao na malalamiko yao, uwatengenezee shauri lao. Tena itakuwa, wakukosee, kwani hakuna mtu asiyekosa, nawe utawakasirikia, uwatie mikononi mwao adui, wawateke na kuwahamisha wakiwapeleka katika nchi ya kwao ya mbali au ya karibu; lakini hapo, watakapojirudia wenyewe mioyoni mwao katika nchi hiyo, walikohamishiwa, basi, hapo watakapokulalamikia tena katika nchi ya uhamisho wao na kusema: Tumekosa, tumekora manza, tumefanya maovu, watakapokurudia hivyo kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote katika nchi ya adui zao, walikowahamisha nako, watakapokuomba na kuielekea nchi yao, uliyowapa baba zao, nao mji, uliouchagua, nayo Nyumba hii, niliyolijengea Jina lako, basi, wewe huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa na uyasikie maombo yao na malalamiko yao, uwatengenezee shauri lao na kuwaondolea walio ukoo wako makosa yao, waliyokukosea, hata mapotovu yao yote, waliyokutendea, kisha uwapatie huruma machoni pao waliowahamisha, wawahurumie! Kwani ndio watu wa ukoo wako na fungu lako, uliowatoa huko Misri katika tanuru ya kuyeyushia vyuma. Uwe macho, upate kuyasikiliza malalamiko ya mtumishi wako na malalamiko yao walio ukoo wako wa Waisiraeli, uwasikie kila, watakapokulilia! Kwani wewe mwenyewe umewatenga na kuwatoa katika makabila yote ya nchini, wawe fungu lako wewe, kama ulivyosema kinywani mwa mtumishi wako Mose, ulipowatoa baba zetu huko Misri, wewe Bwana Mungu. Salomo alipokwisha kumwomba Bwana maombo haya yote na kumlalamikia hivyo, akainuka hapo mbele ya meza ya kumtambikia Bwana, alipokuwa amepiga magoti, mikono yake ikiwa imekunjuliwa na kuelekea mbinguni. Akasimama, akaubariki mkutano wote wa Waisiraeli na kupaza sauti sana akisema: Bwana na atukuzwe, kwa kuwa amewapatia walio ukoo wake wa Waisiraeli kutulia! Yote yakawa, kama alivyosema. Katika maneno yake yote mazuri, aliyoyasema kinywani mwa mtumishi wake Mose, hakutupotelea hata moja. Bwana Mungu wetu awe nasi, kama alivyokuwa na baba zetu, asituache, wala asitutupe, apate kuielekeza mioyo yetu na kwake, tuendelee katika njia zake zote na kuyaangalia maagizo yake na maongozi yake na maamuzi yake, aliyowaagiza baba zetu. Hayo maneno yangu ya kumlalamikia Bwana na yamkalie Bwana Mungu wetu karibu mchana na usiku, amtengenezee mtumishi wake mashauri yake nao walio ukoo wake wa Waisiraeli mashauri yao, kama itakavyowapasa siku kwa siku, kusudi makabila yote ya nchi yapate kujua, ya kuwa Bwana ndiye Mungu, hakuna mwingine tena. Nayo mioyo yenu yote mizima iwe upande wa Bwana Mungu wetu, mwendelee kuyafuata maongozi yake na kuyaangalia maagizo yake kama siku hii ya leo! Kisha mfalme nao Waisiraeli wote pamoja naye wakamtolea Bwana ng'ombe za tambiko. Salomo akatoa ng'ombe 22000 na mbuzi na kondoo 120000 kuwa ng'ombe za tambiko za kumshukuru Bwana. Ndivyo, mfalme na wana wa Isiraeli wote walivyoieua Nyumba ya Bwana. Siku hiyo mfalme alikitakasa kipande cha kati cha ua uliokuwa mbele ya Nyumba ya Bwana, kwani ndiko, alikotolea ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na vilaji vya tambiko na mafuta ya ng'ombe za tambiko za shukrani, kwani ile meza ya shaba ya kutambikia iliyokuwako kule mbele ya Bwana ilikuwa ndogo, haikueneza kabisa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na vilaji vya tambiko na mafuta ya ng'ombe za tambiko za shukrani. Ndivyo, Salomo alivyofanya sikukuu wakati huo, yeye pamoja nao Waisiraeli wote, wakawa mkutano mkubwa wa watu waliotoka Hamati mpaka kwenye mto wa Misri; wakafanya sikukuu mbele ya Bwana siku saba, na tena siku saba, pamoja zilikuwa siku kumi na nne. Siku ya nane akawapa watu ruhusa, wakaagana na mfalme na kumbariki, wakaenda mahemani kwao wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote, Bwana alimfanyizia mtumishi wake Dawidi nao walio ukoo wake wa Waisiraeli. Salomo alipomaliza kuijenga Nyumba ya Bwana na nyumba ya mfalme na kuyafanya yote, Salomo aliyotaka kuyafanya kwa kupendezwa nayo, ndipo, Bwana alipomtokea Salomo mara ya pili, kama alivyomtokea kule Gibeoni. Bwana akamwambia: Nimeyasikia maombo yako na malalamiko yako, uliyonilalamikia; nimeitakasa Nyumba hii, uliyoijenga, nilikalishe Jina langu humu kale na kale, nayo macho yangu pamoja na moyo wangu yatakuwa humu siku zote. Wewe nawe ukiendelea kuwa machoni pangu, kama baba yako Dawidi alivyoendelea kwa moyo ulionyoka wote, uyafanye yote, niliyokuagiza, ukiyaangalia maongozi yangu na maamuzi yangu, ndipo, nitakapokisimamisha kiti cha kifalme cha ufalme wako wa kuwatawala Waisiraeli, kisimame kale na kale, kama nilivyomwambia baba yako Dawidi kwamba: Kwako hakutakoseka mtu atakayekaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli. Lakini mtakaporudi nyuma ninyi au wana wenu, msinifuate, msiyaangalie maagizo yangu na maongozi yangu, niliyoyatoa machoni penu, mkaja kutumikia miungu mingine na kuiangukia, ndipo, nitakapowang'oa Waisiraeli katika nchi hii, niliyowapa, nayo Nyumba hii, niliyoitakasa, iwe Kao la Jina langu, nitaiacha, macho yangu yasiione tena, nao Waisiraeli watakuwa fumbo na simango kwa makabila yote. Nayo Nyumba hii iliyokuwa imetukuka kabisa, basi, kila atakayeipita ataistukia na kuizomea, waulize: Kwa sababu gani Bwana ameifanyizia hivi nchi hii na Nyumba hii? Ndipo, watakapojibu: Kwa kuwa walimwacha Bwana Mungu wao aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine wakaiangukia na kuitumikia; hii ndiyo sababu, Bwana akiwaletea haya mabaya yote. Ile miaka ishirini, ambayo Salomo alizijenga zile nyumba mbili, Nyumba ya Bwana na nyumba ya mfalme, ilipokwisha kupita, ndipo, mfalme Salomo alipompa Hiramu, mfalme wa Tiro, miji ishirini katika nchi ya Galili, kwa kuwa alimpatia mfalme Salomo miti ya miangati na miti ya mivinje na dhahabu, yote pia, kama alivyoitaka. Hiramu alipotoka Tiro kuitazama hiyo miji, Salomo aliyompa, haikumpendeza, akasema: Ni miji gani hii, uliyonipa, ndugu yangu? Wakaiita nchi ya Kabuli hata siku hii ya leo. Naye Hiramu alikuwa amempelekea mfalme vipande 120 vya dhahabu, ndio frasila 360. Kazi za watu, mfalme Salomo aliowatoa kufanya kazi za nguvu, ni hizi: waliijenga Nyumba ya Bwana na nyumba yake na Milo na boma la kuuzunguka Yerusalemu, tena Hasori na Megido na Gezeri. Kwani Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda, akauteka Gezeri, akauteketeza kwa moto, nao Wakanaani waliokaa humo, akawaua, kisha akampa mwanawe aliyekuwa mkewe Salomo, uwe tunzo lake. Lakini Salomo akajenga Gezeri tena, hata Beti-Horoni wa chini, na Balati na Tamari ulioko nyikani katika nchi ile; hata miji yote yenye vilimbiko, Salomo aliyokuwa nayo, nayo miji ya magari na miji ya farasi na majengo yote, Salomo aliyotaka kuyajenga kwa mapenzi yake mle Yerusalemu nake huko Libanoni na katika nchi yo yote ya ufalme wake. Watu, aliowatumia, ndio wote waliosalia wa Waamori na wa Wahiti na wa Waperizi na wa Wahiwi na wa Wayebusi wasiokuwa wa wana wa Isiraeli; wana wao wale waliosalia na kuachwa na wenzao katika nchi hii, kwa kuwa wana wa Isiraeli hawakuweza kuwamaliza na kuwaua kwa kuwatia mwiko wa kuwapo, basi, hawa Salomo akawatoa, akawafanyisha kazi za nguvu za kitumwa hata siku hii ya leo. Lakini wana wa Isiraeli Salomo hakuwataka kuwa watumwa, kwani hawa walikuwa wapiga vita na watumishi wake na wakuu wake na wakuu wa thelathini na wakuu wa magari yake na wapanda farasi wake. Nao wakuu wa mfalme Salomo waliowekwa kusimamia kazi walikuwa 550; ndio waliowatawala watu waliofanya kazi. Binti Farao alipokwisha kutoka katika mji wa Dawidi na kuingia katika nyumba yake, aliyomjengea, ndipo, alipolijenga lile boma lililoitwa Milo. Salomo akatoa kila mwaka mara tatu ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani hapo pa kutambikia, alipomjengea Bwana; kila mara, alipozitoa, akavukiza penye meza iliyoko mbele ya Bwana. Alifanya hivyo alipokwisha kuimaliza hiyo Nyumba. Kisha mfalme Salomo akatengeneza nazo merikebu za mizigo kule Esioni-Geberi karibu ya Eloti huko pwani kwenye Bahari Nyekundu iliyoko katika nchi ya Edomu. Hiramu akatuma watumishi wake wa kutumia merikebuni walio mafundi wa kazi za merikebuni, walioijua nayo bahari, wafanye kazi pamoja na watumishi wa Salomo. Wakaenda Ofiri, wakachukua huko vipande vya dhahabu 420, ndio frasila 1260, wakampelekea mfalme Salomo. Mfalme wa kike wa Saba alipousikia uvumi wa Salomo nayo, aliyolifanyia Jina la Bwana, akaenda kumjaribu kwa maulizo ya kufumbafumba. Akaja Yerusalemu na vikosi vikubwa mno na ngamia waliochukua uvumba na dhahabu nyingi sana na vito. Alipofika kwa Salomo akasema naye na kumwuliza yote, aliyokuwa nayo moyoni mwake. Salomo akamwelezea yote, aliyomwuliza, halikuwako neno lililofichika maana kwake mfalme, asiloweza kumwelezea. Ndipo, mfalme wa kike wa Saba alipouona werevu wa Salomo kuwa wa kweli, kisha akaitazama nyumba, aliyoijenga, na vilaji vilivyopo mezani na vikao vya watumwa wake na kazi za watumishi wake na mavazi yao na watunza vinywaji wake na ng'ombe zake za tambiko za kuteketezwa nzima, alizozipeleka Nyumbani mwa Bwana, ndipo, roho yake ilipozimia, akamwambia mfalme: Kumbe ni ya kweli, niliyoyasikia katika nchi yangu ya mambo yako na ya werevu wako ulio wa kweli! Lakini sikuyaitikia hayo maneno kuwa ya kweli, mpaka nikija, nikayaona kwa macho yangu. Tena naona, ya kuwa sikuambiwa nusu tu, unauzidisha werevu wa kweli na wema, ni mkuu kuliko ule uvumi, niliousikia. Wenye shangwe ni watu wako, nao hawa watumwa wako ni wenye shangwe kwa kusimama mbele yako siku zote na kuyasikia maneno ya werevu wako ulio wa kweli. Bwana Mungu wako na atukuzwe, kwa kuwa alipendezwa na wewe, akakukalisha katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli. Kwa kuwa Bwana anawapenda Waisiraeli kale na kale, alikuweka kuwa mfalme wao, uwaamue kwa wongofu. Kisha akampa mfalme vipande vya dhahabu 120, ndio frasila 360, na uvumba mwingi sana na vito; uvumba mwingi kama huo, mfalme wa kike wa Saba aliompa mfalme Salomo, ulikuwa haujaingia huko bado. Kweli hata merikebu za Hiramu zilizochukua dhahabu huko Ofiri zikaleta toka Ofiri nayo miti ya uvumba mingi sana na vito. Naye mfalme akaitumia hiyo miti ya uvumba ya kuzikingia baraza za Nyumba ya Bwana na za nyumba ya mfalme na ya kutengeneza mazeze na mapango ya waimbaji. Miti ya uvumba kama hiyo ilikuwa haijaingia huko bado, wala haikuonekana tena hata siku hii ya leo. Kisha mfalme Salomo akampa mfalme wa kike wa Saba yote, aliyopendezwa nayo, aliyomwomba; kuyapita hayo mfalme Salomo akampa mwenyewe matunzo, kama ilivyompasa mfalme. Kisha akarudi kwenda kwao katika nchi yake, yeye na watumishi wake. Uzito wa dhahabu, Salomo alizoletewa katika mwaka mmoja ulikuwa vipande vya dhahabu 666, ndio frasila 2000, pasipo zile, alizozitoza watembezi na wachuuzi na wafalme wote wa nchi ya Waarabu na watawala nchi yake. Mfalme Salomo akatengeneza ngao 200 za dhahabu zilizofuliwa, kila ngao moja ikatumiwa sekeli 600, ndio nusu kubwa ya frasila ya dhahabu. Kisha akatengeneza ngao ndogo 300 za dhahabu zilizofuliwa, hizi ngao ndogo kila moja ikatumiwa mane tatu, ndio ratli sita za dhahabu, mfalme akaziweka katika nyumba ya mwituni kwa Libanoni. Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme cha pembe za tembo, akakifunikiza dhahabu zilizong'azwa. Hicho kiti cha kifalme kilikuwa na vipago sita vya kukipandia, tena huko nyuma hicho kiti cha kifalme kilikuwa kimeviringana juu. Tena hapo pa kukalia palikuwa na maegemeo huku na huko, nayo mifano miwili ya simba ilikuwa imesimama hapo penye maegemeo. Tena mifano kumi na miwili ya simba ilikuwa imesimama juu ya vile vipago sita, huku na huko. Kitu kilichotengenezwa vizuri hivyo hakikuwako katika ufalme wote. Navyo vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Salomo vilikuwa vya dhahabu, navyo vyombo vyote vya ile nyumba ya mwituni kwa Libanoni vilikuwa vya dhahabu zilizong'azwa, kwani fedha ziliwaziwa kuwa si kitu katika siku za Salomo. Kwani mfalme alikuwa na merikebu za Tarsisi zilizosafiri baharini pamoja na merikebu za Hiramu, kila miaka mitatu hizo merikebu za Tarsisi zikaja mara moja, zikaleta dhahabu na fedha na pembe za tembo na tumbili na madege wenye manyoya mazuri mno wanaoitwa tausi. Hivyo ndivyo, mfalme Salomo alivyokuwa mkuu kuwapita wafalme wote wa huku nchini kwa utukufu na kwa werevu wa kweli. Watu wa nchi zote wakataka kuuona uso wake Salomo, wayasikie maneno ya werevu wake wa kweli, Mungu alioutia moyoni mwake. Nao wakaleta kila mtu matunzo yake: vyombo vya fedha na vya dhahabu na mavazi na mata na uvumba na farasi na nyumbu; vikawa hivyo mwaka kwa mwaka. Salomo akakusanya magari na wapanda farasi, hata akawa na magari 1400 na wapanda farasi 12000, akawakalisha katika miji ya magari namo mwake mfalme mle Yerusalemu. Mfalme akajipatia fedha kuwa nyingi mle Yerusalemu kama mawe, nayo miti ya miangati akajipatia kuwa mingi kama mitamba katika nchi ya tambarare. Nao farasi, Salomo aliokuwa nao, walitoka Misri, wachuuzi wengi wa mfalme waliwaleta wengi wakiwanunua na kuzilipa bei zao. Magari yaliyokuja kutoka Misri moja lilikuwa fedha 600 na farasi mmoja fedha 150. Vivyo hivyo waliwapelekea nao wafalme wote wa Wahiti na wafalme wa Ushami kwa mikono yao. Mfalme Salomo akapenda wanawake wageni pamoja na binti Farao, wa Kimoabu na wa Kiamoni na wa Kiedomu na wa Kisidoni na wa Kihiti. Wote ni wa wamizimu wale, ambao Bwana aliwaagiza wana wa Isiraeli kwamba: Msiingie kwao, wala wao wasiingie kwenu! Kwani wataigeuza mioyo yenu, mwifuate miungu yao. Wao ndio, Salomo aliogandamana nao kwa kuwapenda. Naye alikuwa na wanawake wa kifalme 700 na masuria 300; hao wakeze ndio waliougeuza moyo wake. Ikawa, Salomo alipokuwa mzee, ndipo, wakeze walipougeuza moyo wake, afuate miungu mingine; kwa hiyo moyo wake haukuwa wote mzima upande wa Bwana Mungu wake, kama moyo wa baba yake Dawidi ulivyokuwa. Salomo akamfuata Astoreti, mungu wa kike wa Sidoni, na Milkomu, tapisho lao Waamoni. Ndivyo, Salomo alivyoyafanya yaliyokuwa mabaya machoni pake Bwana, asipojihimiza kumfuata Bwana kama baba yake Dawidi. Siku zile Salomo akamjengea Kemosi, tapisho lao Wamoabu, kijumba cha kumtambikia juu ya mlima ulioko mbele ya Yerusalemu, hata Moleki, tapisho lao wana wa Amoni. Ndivyo, alivyowafanyia wakeze wageni wote, wapate kuivukizia na kuitambikia miungu yao. Ndipo, Bwana alipomchafukia Salomo, kwa kuwa ameugeuza moyo wake, usimwelekee Bwana Mungu wa Isiraeli aliyemtokea mara mbili. Naye alikuwa amemwagiza neno hilo, asifuate miungu mingine; lakini hakuyashika, Bwana aliyomwagiza. Kwa hiyo Bwana akamwambia Salomo: Kwa kuwa mambo yako yameendelea hivyo, usilishike agano langu, wala usiyafuate maongozi yangu, niliyokuagiza, nitakunyang'anya kweli ufalme, nimpe mtumishi wako. Lakini sitavifanya katika siku zako za kuwapo kwa ajili ya baba yako Dawidi, ila nitaunyang'anya mkononi mwa mwanao. Lakini sio ufalme wote, nitakaomnyang'anya, ila nitampa mwanao shina moja kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi, na kwa ajili ya Yerusalemu, niliouchagua. Bwana akainua mtu, awe mpingani wake Salomo, ni Mwedomu Hadadi aliyekuwa wa kizazi cha mfalme wa Edomu. Ilikuwa siku zile, Dawidi alipowashinda Waedomu; hapo Yoabu, mkuu wa vikosi, alipanda kuwazika waliouawa. Ndipo, alipomwua kila mtu wa kiume aliyepatikana kule Edomu. Kwani Yoabu na Waisiraeli wote walikaa huko miezi sita, mpaka wakiisha kuwaangamiza watu wa kiume wote kule Edomu. Lakini Hadadi alikimbia pamoja na waume wengine wa Edomu waliokuwa watumwa wa baba yake, wakaenda naye Misri, naye Hadai alikuwa akingali kijana mdogo. Wakaondoka Midiani, wakaja Parani, wakachukua watu wengine kule Parani kwenda nao Misri, kisha wakafika Misri kwa Farao, mfalme wa Misri. Huyu akampa nyumba, akamwagizia chakula, akampa nayo mashamba. Hadadi akapata upendeleo kabisa machoni pa Farao, akamwoza ndugu ya mkewe, ndiye ndugu ya Tahapenesi aliyekuwa mkewe mfalme. Huyu ndugu ya Tahapenesi akamzalia mwana wa kiume, Genubati; naye Tahapenesi akamkuza nyumbani mwa Farao. Kwa hiyo Genubati alikuwa nyumbani mwa Farao katikati ya wanawe Farao. Hadadi aliposikia kule Misri, ya kuwa Dawidi amelala na baba zake, tena ya kuwa Yoabu, mkuu wa vikosi, amekufa, ndipo, Hadadi alipomwambia Farao: Nipe ruhusa, niende kwetu katika nchi yangu! Farao akamwambia: Unakosa nini huku kwangu ukitafuta njia ya kwenda katika nchi yako? Akamwambia: Hakuna, lakini nipe ruhusa, nijiendee! Kisha Mungu akamwinua Rezoni, mwana wa Eliada, awe mpingani wake; ni yule aliyetoroka kwa bwana wake Hadadezeri, mfalme wa Soba. Akakusanya watu kwake, akawa mkuu wa kile kikosi, Dawidi alichowaua. Halafu wakaja Damasko, wakakaa huko na kupata ufalme wa Damasko. Akawa mpingani wa Waisiraeli siku zote za maisha yake Salomo. Akayaongeza yale mabaya, Hadadi aliyoyafanya, akachukizwa na Waisiraeli, akawa mfalme wa Ushami. Alikuwako naye Yeroboamu, mwana wa Nebati wa Efuraimu wa mji wa Sereda; jina la mama yake ni Serua aliyekuwa mjane. Yeroboamu alikuwa mtumishi wa Salomo, lakini aliinua mkono kwa kumkataa mfalme. Naye akiinua mkono, amkatae mfalme, ilikuwa kwa ajili ya jambo hili: Salomo alipojenga Milo, apafunge mahali pale palipokuwa wazi penye mji wa baba yake Dawidi, yeye Yeroboamu alikuwa fundi wa vita mwenye nguvu. Salomo alipomwona huyu kijana, alivyofanya kazi, akamweka kuwa msimamizi wa kazi zote za nguvu za mlango wa Yosefu. Ikawa siku moja, Yeroboamu alipotoka Yerusalemu, mfumbuaji Ahia wa Silo akamwona njiani, naye alikuwa amevaa kanzu mpya; nao hao wawili walikuwa peke yao huko mashambani. Ahia akajivua kanzu yake mpya, aliyokuwa ameivaa, akairarua, itoke vipande 12. Akamwambia Yeroboamu: Jitwalie vipande kumi! Kwani ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyokuambia: Utaniona, nikimnyang'anya Salomo ufalme mkononi mwake, nikupe wewe mashina kumi. Shina moja litakuwa lake kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi na kwa ajili ya Yerusalemu, niliouchagua katika mashina yote ya Isiraeli. Kwani wameniacha, wakamtambikia Astoreti, mungu wa Sidoni, na Kemosi, mungu wa Moabu, na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni, hawakuendelea kuzishika njia zangu na kuyafanya yanyokayo machoni pangu na kuyafuata maongozi yangu na maamuzi yangu kama baba yake Dawidi. Lakini sitauondoa ufalme wote mkononi mwake yeye, ila nitamweka kuwa mkuu siku zote za maisha yake kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi, niliyemchagua, aliyeyaangalia maagizo yangu na maongozi yangu. Nitauondoa ufalme mkononi mwa mwanawe, nikupe mashina kumi. Mwanawe nitampa shina moja, kusudi mtumishi wangu Dawidi awe siku zote na taa iwakayo mbele yangu huko Yerusalemu, mle mjini, nilimochagua kuwa mwa kulikalishia humo Jina langu. Lakini wewe nitakuchukua, nikupe kuyatawala yote, roho yako iyatamaniyo, utakuwa mfalme wao Waisiraeli. Kama utayasikia yote, nitakayokuagiza, uzifuate njia zangu na kuyafanya yanyokayo machoni pangu na kuyaangalia maongozi yangu na maagizo yangu, kama mtumishi wangu Dawidi alivyofanya, ndipo, nitakapokuwa na wewe, nikujengee nyumba itakayokuwa yenye nguvu, kama nilivyomjengea Dawidi, nao Waisiraeli nitakupa. Lakini wao wa kizazi cha Dawidi nitawatesa kwa ajili ya mambo hayo, lakini si siku zote. Salomo akataka kumwua Yeroboamu, kwa hiyo Yeroboamu akaondoka, akakimbia kwenda Misri kwa Sisaki, mfalme wa Misri, akawa huko Misri, hata Salomo alipokufa. Mambo mengine ya Salomo nayo yote, aliyoyafanya, na maneno ya werevu wake uliokuwa wa kweli, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya Salomo? Nazo siku, Salomo alizokuwa mfalme mle Yerusalemu na kuwatawala Waisiraeli wote, ni miaka 40. Kisha Salomo akaja kulala na baba zake, akazikwa mjini mwa baba yake Dawidi, naye mwanawe Rehabeamu akawa mfalme mahali pake. Rehabeamu akaenda Sikemu, kwani Waisiraeli wote walifika Sikemu kumpa ufalme. Naye Yeroboamu, mwana wa Nebati, akayasikia, lakini alikuwa angaliko huko Misri, alikokimbilia alipomkimbia mfalme Salomo; huko Misri ndiko, Yeroboamu alikokaa. Walipotuma kumwita, Yeroboamu akaja na mkutano wote wa Waisiraeli, wakamwambia Rehabeamu kwamba: Baba yako alitutwisha mzigo mzito, nawe wewe sasa utupunguzie ule utumwa mgumu wa baba yako nao mzigo wake mzito, aliotutwisha! Kisha tutakutumikia. Akawaambia: Nendeni kwanza siku tatu, kisha rudini kwangu! Watu walipokwenda zao, mfalme Rehabeamu akafanya shauri na wazee waliomtumikia baba yake Salomo, alipokuwa mzima bado, akawauliza: Ninyi shauri lenu ni nini? Watu hawa tuwape majibu gani? Wakamwambia hivi: Ukiwaitikia leo watu hawa na kuwatumikia, tena ukiwajibu na kuwaambia maneno mema, ndipo, watakapokuwa watumishi wako siku zote. Lakini akaliacha shauri la wazee, walilompa, akafanya shauri na vijana waliokua naye na kumtumikia, akawauliza: Ninyi shauri lenu ni nini? tuwape majibu gani watu hawa walioniambia: Tupunguzie mzigo, aliotutwisha baba yako? Vijana hawa waliokua naye wakasemezana naye kwamba: Haya ndiyo, uwaambie watu hao waliokuambia kwamba: Baba yako aliukuza mzigo wetu kuwa mzito, wewe utupuzie huo mzigo wetu, basi uwaambie hivyo: Kidole changu kidogo na kinenepe kuliko viuno vya baba yangu, sasa vitakuwa hivi: kama baba yangu aliwatwisha mzigo mzito, mimi nitauzidisha mzigo wenu; kama baba yangu aliwapiga fimbo, mimi nitawapiga viboko vyenye miiba. Yeroboamu na watu wote wakaja kwake Rehabeamu siku ya tatu, kama mfalme alivyosema kwamba: Rudini kwangu siku ya tatu! Ndipo, mfalme alipowapa hawa watu majibu magumu akiliacha shauri la wazee, walilompa, akasema nao na kulifuata shauri la vijana kwamba: Kama baba yangu aliwatwisha mzigo mzito, mimi nitauzidisha; kama baba yangu aliwapiga fimbo, mimi nitawapiga viboko vyenye miiba. Mfalme hakuwasikia wale watu, kwani Bwana aliyageuza kuwa hivyo, apate kulitimiza neno lake, alilomwambia Yeroboamu, mwana wa Nebati, kinywani mwa Ahia wa Silo. Waisiraeli wote walipoona, ya kuwa mfalme hakuwasikia, ndipo, watu walipomjibu mfalme neno la kwamba: Sisi tuna bia gani na Dawidi? Hatuna fungu lo lote kwake mwana wa Isai. Waisiraeli, haya! Rudini sasa mahemani kwenu! Nawe Dawidi, na uuangalie mwenyewe mlango wako! Ndipo, Waisiraeli walipokwenda mahemani kwao. Ni wana wa Isiraeli waliokaa katika miji ya Yuda tu, Rehabeamu aliowapata, awe mfalme wao. Mfalme Rehabeamu alipomtuma Adoramu aliyekuwa msimamizi wa kazi za nguvu, wana wa Isiraeli wote wakampiga mawe, hata akafa. Kisha mfalme Rehabeamu akajihimiza kupanda garini na kukimbilia Yerusalemu. Ndivyo, Waisiraeli walivyojitenga na mlango wa Dawidi mpaka siku ya leo. Ikawa, Waisiraeli wote waliposikia, ya kuwa Yeroboamu amerudi, wakatuma kumwita kuja kwenya mkutano, wakamfanya kuwa mfalme wa Waisiraeli wote, hakuna aliyeufuata mlango wa Dawidi, ni shina la Yuda peke yake tu. Rehabeamu alipofika Yerusalemu akaukusanya mlango wote wa Yuda na shina la Benyamini, watu 180000 waliochaguliwa kupiga vita, wapigane na mlango wa Waisiraeli, wamrudishie Rehabeamu, mwana wa Salomo, ufalme huo. Lakini neno la Mungu likamjia Semaya aliyekuwa mtu wa Mungu, kwamba: Mwambie Rehabeamu, mwana wa Salomo, mfalme wa Wayuda, nao wote wa milango ya Yuda na ya Benyamini nao wale watu waliosalia huku kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msipande kwenda kupigana na ndugu zenu, wana wa Isiraeli! Rudini kila mtu nyumbani kwake! Kwani jambo hili limefanywa na mimi. Walipolisikia neno hili la Bwana, wakarudi kwenda zao, kama Bwana alivyosema. Yeroboamu akaujenga Sikemu milimani kwa Efuraimu, akakaa humo; kisha akatoka humo, akajenga Penueli. Yeroboamu akasema moyoni mwake: Sasa ufalme utarudi kuwa wa mlango wa Dawidi, watu wa huku wakipanda kwenda kutambikia Nyumbani mwa Bwana mle Yerusalemu; ndipo, mioyo ya watu wa huku itakapowageukia mabwana zao naye Rehabeamu, mfalme wa Wayuda, kisha wataniua, wapate kurudi kwa Rehabeamu, mfalme wa Wayuda. Mfalme alipokwisha kulifanya shauri hilo akatengeneza ndama mbili za dhahabu, akawaambia watu: Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; Waisiraeli, itazameni miungu yenu iliyowatoa katika nchi ya Misri! Ndama moja akaiweka Beteli, moja akaiweka Dani. Jambo hili likawakosesha watu, kwani watu wakaenda hata Dani kuitambikia hiyo moja. Hata vilimani juu akatengeneza vijumba vya kutambikia, akaweka nao watu wo wote kuwa watambikaji wasiokuwa na wana wa Lawi. Yeroboamu akafanya sikukuu katika mwezi wa 8 siku ya 15 ya huo mwezi kama sikukuu ya Wayuda, naye akatoa ng'ombe za tambiko hapo pa kutambikia. Ndivyo, alivyofanya hata Beteli, azitambikie zile ndama, alizotengeneza; kisha akaweka Beteli watambikaji wa kutambika katika vijumba, alivyovijenga vilimani. Napo hapo, alipopatengeneza pa kutambikia huko Beteli, akatoa ng'ombe za tambiko, ikawa ile siku ya 15 ya mwezi wa 8, aliyoizusha moyoni mwake; hapo, alipowafanyia wana wa Isiraeli sikukuu, akapanda kufika hapo pa kutambikia, avukize. Mara akatokea mtu wa Mungu. Naye alitoka Yuda kuja Beteli kwa kuagizwa na Bwana. Akatokea papo hapo, Yeroboamu aliposimama penye meza ya kutambikia, avukize. Kwa kuagizwa na Bwana akapaza sauti kwa ajili ya hiyo meza ya kutambikia, akasema: Meza ya kutambikia! Meza ya kutambikia! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazama! Nyumbani mwa Dawidi atazaliwa mwana, jina lake Yosia; yeye atachinja juu yako kuwa ng'ombe za tambiko watambikaji wa vijumba vya vilimani wanaovukiza juu yako; ndipo, watakapoteketeza juu yako mifupa ya watu. Siku hiyohiyo akawapa hata kielekezo akisema: Hiki ndicho kielekezo, Bwana alichokisema: Mtaona meza hii ya kutambikia ikipasuka, majivu ya mafuta yaliyoko juu yake yamwagike. Mfalme alipolisikia neno hili la yule mtu wa Mungu, alilolisema na kupaza sauti kwa ajili ya meza ya kutambikia ya Beteli, Yeroboamu akaunyosha mkono wake akisimama penye ile meza ya kutambikia, akasema: Mkamateni! Ndipo, mkono wake, aliomnyoshea, ulipokauka, asiweze kuurudisha kwake. Nayo meza ya kutambikia ikapasuka, nayo majivu ya mafuta yaliyokuwa juu yake yakamwagika hapo mezani pa kutambikia; ndicho kielekezo, yule mtu wa Mungu alichowapa kwa kuagizwa na Bwana. Mfalme akaomba na kumwambia yule mtu wa Mungu: Mlalamikie Bwana Mungu wako usoni pake na kuniombea, mkono wangu upate kurudi kwangu! Yule mtu wa Mungu alipomlalamikia Bwana usoni pake, ndipo, mkono wa mfalme uliporudi kwake, ukawa, kama ulivyokuwa kwanza. Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu: Njoo, twende pamoja nyumbani, upate kutulia kidogo, nami nikupe tunzo. Yule mtu wa Mungu akamwambia mfalme: Ijapo, unipe nusu ya nyumba yako, sitakwenda na wewe, wala sitakula mkate, wala sitakunywa maji mahali hapa. Kwani ndivyo, nilivyoagizwa na neno la Bwana kwamba: Usile huko mkate, wala usinywe maji, wala usiirudie njia ile, uliyokwenda nayo! Akaenda zake na kushika njia nyingine, hakuirudia njia ile, aliyokuja nayo alipokwenda Beteli. Huko Beteli alikaa mfumbuaji mzee; wanawe huyu wakaja, wakamsimulia matendo yote, yule mtu wa Mungu aliyoyatenda Beteli siku hiyo, nayo maneno, aliyomwambia mfalme. Walipokwisha kumsimulia haya baba yao, baba yao akawauliza: Amekwenda na kushika njia gani? Wanawe walipomwonyesha njia, yule mtu wa Mungu aliyetoka Yuda aliyoishika, akawaambia wanawe: Nitandikieni punda! Walipkwisha kumtandikia punda, akampanda, akamfuata yule mtu wa Mungu, akamkuta, akikaa chini ya mkwaju, akamwuliza: Kumbe wewe ndiwe mtu wa Mungu aliyetoka Yuda? Akamwambia: Ni mimi. Akamwambia: Nifuate kwenda nyumbani, ule chakula! Akamjibu: Siwezi kurudi na wewe wala kuingia mwako; sitakula chakula kwako, wala sitakunywa maji mahali hapa, kwani nimeambiwa na neno la Bwana: Usile huko chakula, wala usinywe maji huko, wala usirudi na kuishika njia ile, uliyokuja nayo! Ndipo, yule alipomwambia: Mimi mami ni mfumbuaji kama wewe; nami malaika ameniambia kwa kuagizwa na Bwana kwamba: Umrudishe kwako nyumbani, ale chakula, anywe maji! Lakini huko alimwongopea. Akarudi naye, akala chakula nyumbani mwake, akanywa maji. Ikawa, wao walipokaa mezani, ndipo, neno la Bwana lilipomjia yule mfumbuaji aliyemrudisha, akamwambia yule mtu wa Mungu aliyetoka Yuda na kupaza sauti akisema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa kuwa hukukitii kinywa cha Bwana, usiliangalie agizo, Bwana Mungu wako alilokuagiza, ukarudi, ukala chakula, ukanywa maji mahali hapo, alipokuambia: usile chakula, wala usinywe maji hapo! basi, kwa hiyo maiti yako haitaingia kaburini kwa baba zako. Alipokwisha kula chakula na kunywa maji, yule akamtandikia punda huyu mfumbuaji, aliyemrudisha. Alipokwenda zake, simba akamwona njiani, akamwua, nayo maiti yake ikalala njiani hivyo, ilivyoangushwa, naye punda akasimama kando yake, hata simba akasimama kando ya maiti. Mara watu waliopita wakaiona maiti, ilivyolala njiani, naye simba aliyesimama kando yake maiti, wakaja, wakayasimulia mle mjini, yule mfumbuaji mzee alimokaa. Yule mfumbuaji aliyemrudisha njiani alipoyasikia akasema: Huyu ni yule mtu wa Mungu asiyekitii kinywa cha Bwana; kwa hiyo Bwana amemtolea simba, amwue na kumvunjavunja kwa neno la Bwana, alilomwambia. Kisha akawaambia wanawe kwamba: Nitandikieni punda! Wakamtandikia. Alipokwenda, akaiona ile maiti, ilivyolala njiani, punda na simba wakisimama kando ya maiti; yule simba hakuila hiyo maiti, wala hakumrarua punda. Mfumbuaji akaichukua maiti ya yule mtu wa Mungu, akaiweka juu ya punda, akairudisha, aje nayo mjini mwake mfumbuaji mzee, amwombolezee, kisha amzike. Alipokwisha kuilaza maiti kaburini kwake, wakaiombolezea kwamba: A, ndugu yangu! Alipokwisha kumzika, akawaambia wanawe kwamba: Nitakapokufa, sharti mnizike humu kaburini, yule mtu wa Mungu alimozikwa, mifupa yangu mwilaze kando ya mifupa yake. Kwani litatimia kweli lile neno, alilolisema na kupaza sauti kwa kuagizwa na Bwana kwa ajili ya meza ya kutambikia iliyoko Beteli na kwa ajili ya vijumba vyote vya kutambikia vilivyoko vilimani juu katika miji ya Samaria. Lakini hayo yalipofanyika, Yeroboamu hakurudi na kuiacha njia yake mbaya, akaweka tena watu wo wote kuwa watambikaji wa vilimani; aliyependezwa naye akamjaza gao, awe mtambikaji wa vilimani. Neno hilo ndilo lilioukosesha mlango wa Yeroboamu, likauangamiza na kuutowesha huku nchini. Siku zile Abia, mwana wa Yeroboamu, akaugua. Ndipo, Yeroboamu alipomwambia mkewe: Inuka, Ujigeuzegeuze, watu wasikujue, ya kuwa ndiwe mkewe Yeroboamu; kisha nenda Silo! Tazama, huko yuko mfumbuaji Ahia aliyeniambia, ya kama nitakuwa mfalme wao walio ukoo huu. Mkononi mwako uchukue mikate kumi na maandazi na kibuyu chenye asali, uende kwake! Yeye atakuambia yatakayokuwa ya huyu mtoto. Mkewe Yeroboamu akafanya hivyo, kisha akaondoka, akaenda Silo, akaingia nyumbani mwa Ahia; lakini Ahia hakuweza kuona, kwani macho yake yalikuwa yametenda kiwi kwa ajili ya uzee wake. Lakini Bwana alikuwa amemwambia: Tazama, mkewe Yeroboamu anakuja kukuuliza kwa ajili ya mwanawe, kwani yeye ni mgonjwa; nawe umwambie haya na haya! Naye atakapoingia atakuwa amejigeuzageuza kuwa kama mgeni. Ikawa, Ahia aliposikia mashindo ya miguu yake, akiingia mlangoni, akamwambia: Karibu, mke wa Yeroboamu! Mbona unajigeuzageuza kuwa kama mgeni? Nami nimetumwa kukuambia neno gumu. Nenda, umwambie Yeroboamu: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Nimekutoa katikati ya watu, nikakukweza, nikakupa kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli, nikaunyang'anya mlango wa Dawidi ufalme, nikakupa wewe; lakini hukuwa kama mtumishi wangu Dawidi aliyeyaangalia maagizo yangu, akaendelea kunifuata kwa moyo wake wote mzima, ayafanye hayo tu yanyokayo machoni pangu. Lakini umefanya mabaya kuliko wote waliokuwa mbele yako, kwani umejiendea, ukajitengenezea miungu mingine na vinyago, unikasirishe, ukanitupa nyuma yako. Lakini mtaniona, nikiuletea mlango wa Yeroboamu mabaya, niwatoweshe wa kiume walio wa Yeroboamu, kama watakuwa wamefungwa au kama watakuwa wamefunguliwa kwao Waisiraeli, nitawazoa walio wa mlango wa Yeroboamu, kama watu wanavyozoa mavi, hata wamalizike kabisa. Wao wa Yeroboamu watakaokufa mjini mbwa watawala; nao watakaokufa shambani madege wa angani watawala, kwani Bwana amevisema. Nawe inuka, uende nyumbani kwako! Hapo, miguu yako itakapoingia mjini, papo hapo mtoto atakufa. Waisiraeli wote watamwombolezea, kisha watamzika, kwani kwao wa Yeroboamu huyu peke yake ndiye atakayeingia kaburini, kwani katika mlango wa Yeroboamu ni kwake tu kulikoonekana yaliyokuwa mema machoni pa Bwana. Yeye Bwana atajiinulia mfalme wa Waisiraeli atakayeutowesha huu mlango wa Yeroboamu siku hiyo, nayo ya sasa siyo yayo hayo? Ndipo, Bwana atakapowapiga Waisiraeli, kama matete yanavyotikiswa majini; atawang'oa Waisiraeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, awatawanye ng'ambo ya lile jito kubwa, kwa kuwa wamejitengenezea miti ya Ashera inayomkasirisha Bwana. Atawatoa Waisiraeli kwa ajili ya makosa, Yeroboamu aliyoyakosa na kuwakosesha Waisiraeli nao. Kisha mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda zake kufika Tirsa; alipoingia penye kizingiti cha nyumba, ndipo, yule kijana alipokufa. Wakamzika, nao Waisiraeli wote wakamwombolezea, kama Bwana alivyosema kinywani mwa mtumishi wake mfumbuaji Ahia. Mambo mengine ya Yeroboamu, jinsi alivyopiga vita, tena alivyotawala, tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli. Siku, Yeroboamu alizokuwa mfalme, ni miaka 22; kisha akaja kulala na baba zake, naye mwanawe Nadabu akawa mfalme mahali pake. Rehabeamu, mwana wa Salomo, akapata kuwa mfalme wa Wayuda; yeye Rehabeamu alikuwa mwenye miaka 41 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 17 mle Yerusalemu katika ule mji, Bwana aliouchagua katika mashina yote ya Isiraeli, alikalishe Jina lake humo. Jina la mama yake ni Nama aliyekuwa Mwamoni. Wayuda wakayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, wakamchokoza kwa makosa yao, waliyoyakosa, maana yalikuwa mabaya kuliko yote, baba zao waliyoyafanya. Nao wakajijengea vijumba vya kutambikia vilimani, wakajitengenezea nguzo za kutambikia na miti ya Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wenye majani mengi. Hata wagoni wa patakatifu pao walikuwako katika nchi, wakayafanya matapisho yote ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele yao Waisiraeli. Katika mwaka wa tano wa mfalme Rehabeamu ndipo, Sisaki, mfalme wa Misri, alipopanda kuujia Yerusalemu. Akavichukua vilimbiko vya Nyumbani mwa Bwana navyo vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme, vyote pia akavichukua, nazo ngao za dhahabu, Salomo alizozitengeneza, akazichukua. Mahali pao mfalme Rehabeamu akatengeneza ngao za shaba, akazitia mikononi mwa wakuu wa wapiga mbio waliongoja pa kuingia nyumbani mwa mfalme, waziangalie. Kila mara, mfalme alipoingia Nyumbani mwa Bwana, wapiga mbio wakazichukua, kisha wakazirudisha chumbani mwao wapiga mbio. Mambo mengine ya Rehabeamu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Navyo vita vya kupigana kwao Rehabeamu na Yeroboamu vilikuwako siku zote. Rehabeamu akaja kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa Dawidi, nalo jina la mama yake ni Nama aliyekuwa Mwamoni. Naye mwanawe Abiamu akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 18 wa mfalme Yeroboamu, mwana wa Nebati, Abiamu akapata kuwa mfalme wa Wayuda. Akawa mfalme miaka 3 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Maka, binti Abisalomu. Akaendelea kuyafanya makosa yote ya baba yake, aliyoyafanya machoni pake, nao moyo wake haukuwa wote mzima upande wa Bwana Mungu wake kama moyo wa baba yake Dawidi. Lakini kwa ajili ya Dawidi Bwana Mungu wake akampa kuwa taa iwakayo mle Yerusalemu, akimwinulia mwanawe wa kumfuata, tena akiuacha Yerusalemu, usimame vivyo hivyo. Kwani Dawidi aliyafanya yanyokayo machoni pake Bwana, tena yote aliyomwagiza hakuyaacha siku zote za maisha yake, lisipokuwa lile jambo la Mhiti Uria. Vita vya kupigana kwao Rehabeamu na Yeroboamu vikawako siku zote za maisha yake. Mambo mengine ya Abiamu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Yuda? Navyo vita vya kupigana kwao Abiamu na Yeroboamu vikawako. Abiamu akaja kulala na baba zake, wakamzika mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Asa akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 20 wa Yeroboamu, mfalme wa Waisiraeli, Asa akapata kuwa mfalme wa Wayuda. Akawa mfalme miaka 41 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Maka, binti Abisalomu. Asa akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama baba yake Dawidi. Akawatowesha wagoni wa patakatifu katika nchi yake, hata magogo yote ya kutambikia, baba zake waliyoyatengeneza, akayaondoa. Naye mama yake Maka akamwondoa katika ukuu wake, kwa kuwa alitengeneza kinyago cha Ashera, nacho hicho kinyago chake Asa akakikatakata,, akakiteketeza penye kijito cha Kidoroni. Lakini matambiko ya vilimani hayakutoweka, lakini moyo wake Asa ulikuwa wote mzima upande wa Bwana siku zake zote. Navyo, baba yake alivyovitakasa, pamoja navyo, alivyovitakasa mwenyewe, fedha na dhahabu na vyombo, akavipeleka Nyumbani mwa Bwana. Vita vya kupigana kwao Asa na Basa, mfalme wa Waisiraeli, vikawako siku zao zote. Basa, mfalme wa Waisiraeli, akapanda kuijia nchi ya Yuda, akajenga Rama, asipatikane mtu anayeweza kutoka wala kuingia kwa Asa, mfalme wa Wayuda. Ndipo, Asa alipozichukua fedha zote na dhahabu zilizosalia katika vilimbiko vya Nyumba ya Bwana navyo vilimbiko vya nyumba ya mfalme, akavitia mikononi mwa watumishi wake; kisha mfalme Asa akawatuma kwa Benihadadi, mwana wa Taburimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Ushami, aliyekaa Damasko, kumwambia: Liko agano, tuliloliagana mimi na wewe, naye baba yangu na baba yako; kwa hiyo ninatuma kwako matunzo ya fedha na ya dhahabu. Nenda, ulivunje agano, uliloliagana na Basa, mfalme wa Waisiraeli, aondoke kwangu! Benihadadi akamwitikia mfalme Asa, akawatuma wakuu wa vikosi vyake, alivyokuwa navyo, kwenda kupigana na miji ya Waisiraeli, akaipiga miji ya Iyoni na Dani na Abeli-Beti-Maka na Kineroti yote, hata nchi yote ya Nafutali. Basa alipoyasikia haya akaacha kuujenga Rama, akaja kukaa Tirsa. Ndipo, mfalme Asa alipowapigia Wayuda wote mbiu kwamba: Hakuna asiyepaswa na kazi yangu. Kwa hiyo wakayachukua mawe ya huko Rama nayo miti yake, Basa aliyoitumia ya kujenga, naye mfalme Asa akaitumia ya kujenga Geba wa Benyamini na Misipa. Mambo mengine yote ya Asa na matendo yake ya vitani yenye nguvu, hayo yote, aliyoyafanya, nayo miji aliyoijenga, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Lakini alipokuwa mzee akaugua miguu yake. Kisha Asa akaja kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Yosafati akawa mfalme mahali pake. Nadabu, mwana wa Yeroboamu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli katika mwaka wa pili wa Asa, mfalme wa Wayuda; akawa mfalme wa Waisiraeli miaka 2. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, akaendelea kuishika njia ya baba yake na kuyafanya makosa yake, yaliyowakosesha Waisiraeli. Naye Basa, mwana wa Ahia, wa mlango wa Isakari, akamlia njama, kisha Basa akampiga kule Gibetoni ulioko kwa Wafilisti, yeye Nadabu na Waisiraeli wote walipokuwa wanausonga Gibetoni kwa kuuzinga. Basa akamwua katika mwaka wa tatu wa Asa, mfalme wa Wayuda, akawa mfalme mahali pake. Naye alipokwisha kuwa mfalme akawaua wote waliokuwa wa mlango wa Yeroboamu, hakusaza hata mmoja aliyevuta pumzi kwao wa Yeroboamu, akawamaliza kabisa, kama Bwana alivyosema kinywani mwa mtumishi wake Ahia wa Silo, kwa ajili ya makosa, Yeroboamu aliyoyakosa na kuwakosesha Waisiraeli; ndivyo, alivyomchafua sana Bwana Mungu wa Waisiraeli. Mambo mengine ya Nadabu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Vita vya kupigana kwao Asa na Basa, mfalme wa Waisiraeli, vikawako siku zao zote. Katika mwaka wa tatu wa Asa, mfalme wa Wayuda, Basa, mwana wa Ahia, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli wote huko Tirsa, akawatawala miaka 24. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, akaendelea kuishika njia ya Yeroboamu na kuyafanya makosa yake yaliyowakosesha Waisiraeli. Neno la Bwana likamjia Yehu, mwana wa Hanani, kwa ajili ya Basa kwamba: Nilikukweza na kukutoa uvumbini, nikakupa kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli, lakini umeendelea kuishika njia ya Yeroboamu, ukawakosesha walio ukoo wangu wa Waisiraeli, upate kunichafua kwa makosa yao. Kwa hiyo utaniona, nikimzoa Basa pamoja na mlango wake, nikiutoa mlango wako, uwe kama mlango wa Yeroboamu, mwana wa Nebati. Wao wa Basa watakaokufa mjini mbwa watawala; nao watakaokufa shambani madege wa angani watawala. Mambo mengine ya Basa nayo, aliyoyafanya, nayo matendo yake ya vitani yenye nguvu hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Basa akaja kulala na baba zake, akazikwa Tirsa, naye mwanawe Ela akawa mfalme mahali pake. Neno lile, Bwana alilolitoa kinywani mwa mfumbuaji Yehu, mwana wa Hanani, la mambo yatakayompata Basa na mlango wake, alilisema kwa ajili ya mabaya yote, aliyoyafanya machoni pa Bwana, amchafue kwa matendo ya mikono yake, akiwa kama wao wa mlango wa Yeroboamu, tena kwa kuwa aliwaua wao wa mlango wake. Katika mwaka wa 26 wa Asa, mfalme wa Wayuda, Ela, mwana wa Basa, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli huko Tirsa miaka 2. Ndipo, mtumishi wake Zimuri, mkuu wa nusu ya magari, alipomlia njama; naye alikaa Tirsa. Siku moja alipokunywa na kulewa nyumbani mwa Arsa aliyekuwa mkuu wa nyumbani huko Tirsa, Zimuri akaingia, akampiga na kumwua katika mwaka wa 27 wa Asa, mfalme wa Wayuda, kisha akawa mfalme mahali pake. Alipokwisha kuwa mfalme na kukaa katika kiti chake cha kifalme, akawaua wote waliokuwa wa mlango wa Basa, hakusaza wa kiume hata mmoja, wala ndugu zake, wala rafiki zake. Ndivyo, Zimuri alivyouangamiza mlango wa Basa, kama Bwana alivyosema kinywani mwa mfumbuaji Yehu yatakayompata Basa kwa ajili ya makosa yote ya Basa na kwa ajili ya makosa ya mwanawe Ela, waliyoyakosa na kuwakosesha Waisiraeli, wamchafue Bwana Mungu wa Isiraeli kwa mambo yao yasiyokuwa na maana. Mambo mengine ya Ela nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Katika mwaka wa 27 wa Asa, mfalme wa Wayuda, Zimuri akapata kuwa mfalme huko Tirsa siku 7; nao watu walikuwa wakiuzinga Gibetoni ulioko kwa Wafilisti. Wale watu waliouzinga huo mji waliposikia kwamba: Zimuri amemlia mfalme njama, akamwua, siku hiyo Waisiraeli wote waliokuwa huko makambini wakamfanya Omuri, mkuu wa vikosi, kuwa mfalme wa Waisiraeli. Kisha Omuri pamoja na Waisiraeli wote wakatoka Gibetoni, wakapanda, wausonge Tirsa kwa kuuzinga. Zimuri alipoona, ya kuwa mji umetekwa, akaingia ngomeni nyumbani mwa mfalme, akaichoma moto hiyo nyumba ya mfalme, alimokuwa, akafa hivyo kwa ajili ya makosa yake, aliyoyakosa na kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana akiendelea kuishika njia ya Yeroboamu na kuyafuata makosa yake, aliyoyafanya ya kuwakosesha Waisiraeli. Mambo mengine ya Zimuri nayo njama yake, aliyomlia mfalme, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Siku zile wao walio ukoo wa Waisiraeli wakagawanyika kuwa pande mbili: nusu ya watu ikawa upande wa Tibuni, mwana wa Ginati, wamfanye kuwa mfalme, nusu yao ikawa upande wa Omuri. Lakini watu waliokuwa upande wa Omuri wakapata nguvu kuliko wale waliokuwa upande wa Tibuni, mwana wa Ginati. Tibuni alipokufa, Omuri akaupata ufalme. Katika mwaka wa 31 wa Asa, mfalme wa Wayuda, Omuri akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli miaka 12. Alipoushika ufalme mle Tirsa miaka sita akaununua mlima wa Samaria kwa Semeri na kumlipa vipande viwili vya fedha, ndio shilingi 24000, kisha akajenga mji huko mlimani; nao huo mji, alioujenga, akauita Samaria kwa jina la Semeri aliyekuwa mwenye huo mlima. Omuri akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, naye akafanya mabaya zaidi kuliko wote waliokuwa mbele yake. Akaendelea kuzishika njia zote za Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kuyafanya makosa yake yaliyowakosesha Waisiraeli, wamchafue Bwana Mungu wa Isiraeli kwa mambo yao yasiyokuwa na maana. Mambo mengine ya Omuri, aliyoyafanya, nayo matendo yake ya vitani yenye nguvu, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Omuri akaja kulala na baba zake, akazikwa mle Samaria, naye mwanawe Ahabu akawa mfalme mahali pake. Ahabu, mwana wa Omuri, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli katika mwaka wa 38 wa Asa, mfalme wa Wayuda. Naye Ahabu, mwana wa Omuri, akawa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 22. Ahabu, mwana wa Omuri, akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kuliko wote waliokuwa mbele yake. Tena haikumtoshea kuendelea kuyafanya makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, akamwoa naye Izebeli, binti Etibaali, mfalme wa Sidoni, kisha akaenda kumtumikia Baali na kumwangukia. Akampatia Baali pa kumtambikia katika nyumba ya Baali, aliyoijenga Samaria. Kisha Ahabu akatengeneza hata kinyago cha Ashera; ndivyo, Ahabu alivyozidisha kufanya mambo ya kumchafua Bwana Mungu wa Isiraeli kuliko wafalme wote wa Waisiraeli waliokuwa mbele yake. Hizo siku zake Hieli wa Beteli akaujenga tena mji wa Yeriko. Alipoiweka misingi yake, Abiramu, mwanawe wa kwanza, akafa, tena alipoyatia malango, akafa mwanawe mdogo Segubu, kama Bwana alivyosema kinywani mwa Yosua, mwana wa Nuni. Elia wa Tisibe aliyekaa ugenini huko Gileadi akamwambia Ahabu: Hivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli, ninayemtumikia, alivyo Mwenye uzima, miaka hii umande hautakuwako, wala mvua haitakunya, isipokuwa kwa neno la kinywa changu. Kisha neno la Bwana likamjia la kwamba: Ondoka hapa, ujiendee upande wa maawioni kwa jua kijificha kwenye kijito cha Kriti kinachoingia Yordani! Na unywe katika kijito hicho, tena nimeagiza makunguru, wakutunze kuko huko. Ndipo, alipokwenda, afanye, kama Bwana alivyomwagiza, akaenda kukaa kwenye kijito cha Kriti kinachoingia Yordani. Makunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, tena mkate na nyama jioni, akanywa maji ya hicho kijito. Ikawa, siku zilipopita, kijito kikakauka, kwani hakuna mvua katika nchi. *Ndipo, neno la Bwana lilipomjia la kwamba: Inuka, uende Sareputa katika nchi ya Sidoni, ukae huko! Utaona huko mwanamke mjane, niliyemwagiza, akutunze. Akainuka, akaenda Sareputa. Alipofika penya lango la mji akaona huko mwanamke mjane aliyeokota kuni, akamwita na kumwambia: Uniletee maji kidogo katika kata, ninywe! Alipokwenda kuyaleta, akamwita na kumwambia: Uniletee hata kipande kidogo cha mkate mkononi mwako. Akamjibu: Hivyo, Bwana Mungu wako alivyo Mwenye uzima, sinacho kilichochomwa! Nilivyo navyo ndio gao la unga katika kitungi na vifuta vichache katika kichupa. Tazama, ninaokota vikuni viwili, nije nijipikie mwenyewe na mwanangu, tule, kisha tufe. Elia akamwambia: Usiogope! Nenda, ufanye, kama ulivyosema! Lakini kwanza unitengenezee kiandazi kidogo, uniletee hapa nje! Kisha ujitengenezee wewe na mwanao! Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Unga hautaisha katika kitungi, wala kichupa hakitakosa mafuta mpaka siku ile, Bwana atakaponyesha mvua katika nchi. Yule mwanamke akenda, akafanya, kama Elia alivyosema, akala yeye, naye Elia aliyekuwamo nyumbani mwake siku kwa siku. Lakini unga haukuisha katika kitungi, wala kichupa hakikukosa mafuta, kama Bwana alivyosema kinywani mwa Elia.* Ikawa, hayo yalipokwisha kufanyika, mwanawe huyu mwanamke aliyekuwa mwenye nyumba akaugua, nao ugonjwa wake ukawa wenye nguvu sana, hata pumzi hasikusalia mwilini mwake. Ndipo, mwanamke alipomwambia Elia: Tuko na bia gani mimi na wewe, mtu wa Mungu? Umeingia mwangu kuyaumbua mabaya yangu, niliyoyafanya, umwue mwanangu. Elia akamwambia: Nipe mwanao! Akamchukua kifuani pake, akapanda naye darini, alimokuwa anakaa, akamlaza kitandani pake. Akamlilia Bwana kwamba: Bwana Mungu wangu, mbona umemfanyizia vibaya naye huyu mwanamke, ambaye nimefikia kwake, ukimwua mwanawe? Akamkumbatia mtoto mara tatu na kumlalia juu, akamlilia Bwana akisema: Bwana Mungu wangu, roho ya huyu mtoto na irudi mwake! Bwana akaiitikia sauti ya Elia, roho ya mtoto ikarudi mwilini mwake, akawa mzima tena. Ndipo, Elia alipomchukua mtoto, akashuka naye nyumbani kutoka darini, akampa mama yake yeye Elia akimwambia: Tazama, mwanao ni mzima! Yule mwanamke akamwambia Elia: Sasa hivi nimetambua, ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, nalo Neno la Mungu lililomo kinywani mwako ni la kweli. Siku zilipopita nyingi, neno la Bwana likamjia Elia katika mwaka wa tatu kwamba: Nenda kumtokea Ahabu! Kwani nitanyesha mvua katika nchi. Ndipo, Elia alipokwenda kumtokea Ahabu, lakini njaa ilikuwa ngumu huko Samaria. Ahabu akamwita Obadia, mtumishi wake wa nyumbani, naye Obadia alikuwa mtu aliyemwogopa Bwana kabisa. Hapo, Izebeli alipowaangamiza wafumbuaji wa Bwana, Obadia alichukua wafumbuaji mia, akawaficha hamsini hamsini pangoni, akawatunza na kuwapa mikate na maji. Ahabu akamwambia Obadia: Tembea katika nchi kwenye chemchemi zote za maji na kwenye vijito kutazama-tazama, kama majani yanapatikana ya kuwaponya farasi na punda njaa, tusifiwe na hawa nyama wote. Wakajigawanyia nchi ya kupitia, Ahabu akashika njia moja peke yake, naye Obadia akashika njia nyingine peke yake. Obadia alipofika njiani, mara akakutana na Elia; alipomtambua akamwangukia usoni pake, akamwambia: Kumbe wewe ndiwe bwana wangu Elia! Akamjibu: Ndimi! Nawe nenda, kamwambie bwana wako: Elia ameoneka! Akajibu: Nimekosa nini, wewe ukimtia mtumishi wako mkononi mwa Ahabu, aniue? Hivyo, Bwana Mungu wako alivyo Mwenye uzima, hakuna taifa wala ufalme, bwana wangu asikotuma watu, wakutafute, nao walipomwambia: Hayuko! akawaapisha wenye ufalme, hata mataifa, ya kuwa hawakukuona. Na sasa wewe unasema: Nenda, kamwambie bwana wako: Elia ameoneka! Nami nitakapokwenda kutoka kwako, kisha Roho ya Bwana itakupeleka mahali, nisipopajua, nami nikienda kumpasha Ahabu hiyo habari, basi, asipokuona hataniua? Nami mtumishi wako ninamwogopa Bwana tangu ujana wangu. Wewe bwana wangu, hukuambiwa niliyoyafanya, Izebeli alipowaua wafumbuaji wa Bwana, ya kuwa mia yao hao wafumbuaji wa Bwana nimewaficha hamsini hamsini pangoni, nikawapa mikate na maji? Na sasa wewe unasema: Nenda, kamwambie bwana wako: Elia ameoneka! Ndipo, akaponiua. Elia akamwambia: Hivyo, Bwana Mwenye vikosi, ninayemtumikia, alivyo Mwenye uzima, leo hivi nitamtokea. Basi, Obadia akaenda kukutana na Ahabu, akampasha habari hiyo. Ndipo, Ahabu alipokwenda kukutana na Elia. Ikawa, Ahabu alipomwona Elia, Ahabu akamwambia: Je? Wewe siwe uwaponzaye Waisiraeli? Akajibu: Mimi sikuwaponza Waisiraeli, ila ndiwe wewe pamoja na mlango wa baba yako, mkiyaacha maagizo ya Bwana kwa kuyafuata Mabaali. Sasa tuma, uwakusanye Waisiraeli wote kwangu mlimani kwa Karmeli pamoja na wale wafumbuaji wa Baali 450 nao wale wafumbuaji wa Ashera 400 wanokula mezani kwa Izebeli! Ndipo, Ahabu alipotuma kuwaita wana wa Isiraeli wote, nao wafumbuaji akawakusanya mlimani kwa Karmeli. Elia akafika huko, watu wote waliko, akawaambia: Mpaka lini mtakwenda na kuchechemea pande mbili? Kama Bwana ni Mungu, mfuateni! Kama Baali ni Mungu, mfuateni! Lakini watu hawakumjibu neno. Ndipo, Elia alipowaambia wale watu: Mimi nimesalia peke yangu kuwa mfumbuaji wa Bwana, lakini wafumbuaji wa Baali ni watu 450. Na tupewe ng'ombe wawili, nao wajichagulie dume mmoja, wamkatekate, wamweke juu ya chungu ya kuni, lakini wasitie moto! Nami nitamfanyizia yule dume mwingine vivyo hivyo, kisha nimweke juu ya chungu ya kuni, lakini moto sitatia. Ninyi litambikieni jina la mungu wenu, nami nilitambikie Jina la Bwana. Naye atakayeitikia na kuwakisha moto, yeye ndiye Mungu! Watu wote wakaitikia wakisema: Neno hili ni jema. Kisha Elia akawaambia watambikaji wa Baali: Jichagulieni dume mmoja, mwanze kumtengeneza! Kwani ninyi m wengi. Kisha litambikieni jina la mungu wenu, lakini moto msitie! Wakamchukua yule dume waliyepewa, wakamtengeneza, wakalitambikia jina la Baali kuanzia asubuhi, hata jua likawa kichwani, wakiomba: Baali, tuitikie! Lakini hakuna sauti, wala aitikiaye. Wakarukaruka na kupazunguka hapo pa kutambikia, walipopatengeneza. Jua lilipokuwa kichwani, Elia akawafyoza na kuwaambia: Mwiteni na kupaza sauti! Kwani ni mungu! Labda anafikiri neno, au ametoka, au yuko njiani, labda amelala, sharti aamke! Wakapaza sauti sana za kumwita, wakajichanjachanja kwa mapanga na kwa visu kama desturi yao, hata damu zikawatoka. Saa sita zilipopita, wakawa kama wenye wazimu hata hapo, vilaji vya tambiko vinapotolewa, lakini hakuna sauti, wala hakuna aitikiaye, wala hakuna asikiaye. Ndipo, Elia alipowaambia watu wote: Njoni kwangu! Watu wote walipofika kwake, akapajenga tena hapo pa kumtambikia Bwana palipokuwa pamebomolewa. Elia akachukua mawe 12 kwa hesabu ya mashina ya wana wa Yakobo, ambaye neno la Bwana lilimjia la kwamba: Jina lako litakuwa Isiraeli. Hayo mawe akayajenga na kulitaja Jina la Bwana, pawe pa kutambikia, kisha akachimba mfereji wenye upana wa shamba litoshalo kumyagia humo pishi mbili za mbegu, ukapazunguka hapo pa kutambikia. Kisha akatandika kuni, akamkatakata dume lake la ng'ombe, akamweka juu ya zile kuni. Akasema: Jazeni mitungi minne maji, myamwage juu ya ng'ombe ya tambiko na juu ya kuni! Kisha akasema: Ongezeni mara ya pili! Wakaongeza mara ya pili! akasema tena: Mara ya tatu! Wakaongeza mara ya tatu. Maji yakaenea po pote hapo penye kutambikia, hata mfereji ukajaa maji. Walipotolea vilaji vya tambiko, mfumbuaji Elia akatokea, akasema: Bwana, Mungu wa Aburahamu na wa Isaka na wa Isiraeli, leo hivi na yajulikane, ya kuwa wewe ndiwe Mungu kwao Waisiraeli, mimi nami ndimi mtumishi wako. Tena kwa neno lako nimeyafanya haya yote. Niitikie, Bwana! Niitikie! Ndivyo, watu hawa watakavyojua, ya kuwa wewe Bwana ndiwe Mungu, ya kuwa wewe ndiwe anayeigeuza mioyo yao, wakufuate. Ndipo, moto wa Bwana ulipoanguka, ukaila ng'ombe ya tambiko, hata kuni na mawe na mavumbi, hata maji yaliyokuwa katika mfereji ukayakausha. Watu wote walipoyaona wakaanguka nyusoni pao wakisema: Bwana ndiye Mungu! Bwana ndiye Mungu! Ndipo, Elia alipowaambia: Wakamateni wafumbuaji wa Baali, kwao asipone hata mmoja! Walipowakamata, Elia akawatelemsha kwenye kijito cha Kisoni, akawaua huko. Elia akamwambia Ahabu: Nenda, ule, unywe! Kwani nasikia uvumi wa mvua. Ahabu alipokwenda zake huko juu kula na kunywa, Elia akapanda Karmeli pembeni, akainama chini na kuuweka uso magotini. Akamwambia kijana, aliyekuwa naye: Panda, uchungulie upande wa baharini! Akapanda, akapachungulia, akasema: Hakuna ninachokiona, akamwambia: Rudi mara saba! Alipofika mara ya saba akasema: Nimeona kiwingu kidogo kama kiganja cha mtu, kinatoka baharini. Akamwambia: Nenda kumwambia Ahabu: Tandika farasi, ushuke upesi, mvua isikuzuie! Punde si punde, mara mbingu ikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua kubwa. Ahabu akapanda garini, akaja Izireeli. Lakini mkono wa Bwana ukamjia Elia, akajifunga viuno vyake, akapiga mbio kwenda mbele ya Ahabu mpaka kufika Izireeli. Ahabu akamsimulia Izebeli yote, Elia aliyoyafanya, na jinsi alivyowaua wafumbuaji wote wa Baali. Ndipo, Izebeli alipotuma mjumbe kwake Elia kumwambia: Mungu na anifanyizie hivi, tena hivi, nisipoifanyizia roho yako kuwa kesho wakati huuhuu kama roho yake mmoja wao! Ndipo, aliposhikwa na woga, akaondoka, akaenda zake. Alipofika Beri-Seba ulioko katika nchi ya Yuda akamwacha huko kijana, aliyekuwa naye. Mwenyewe akaenda nyikani mwendo wa siku moja, akaja kukaa chini ya mfagio mmoja, akajiombea kufa akisema: Nimechoka sasa; Bwana, ichukue roho yangu! Kwani mimi si mwema kuliko baba zangu. Kisha akalala usingizi penye huo mfagio mmoja. Mara malaika akamgusa, akamwambia: Inuka, ule! Alipotazama akaona kichwani kwake mkate uliochomwa na kibuyu cha maji; akala, akanywa, kisha akarudi, akalala. Ndipo, malaika wa Bwana aliporudi mara ya pili, akamgusa na kumwambia: Inuka, ule! Kwani njia, utakayokwenda, ni ndefu ya kuzishinda nguvu zako. Akainuka, akala, akanywa. Kisha akaenda kwa nguvu ya hicho chakula siku 40 mchana na usiku, mpaka akiufikia mlima wa Mungu, jina lake Horebu. Akaingia huko pangoni, akalala mle. Ndipo, neno la Bwana lilipomjia la kumwuliza: Unafanya nini humu, Elia? Akajibu: Nimejihimiza sana kwa ajili ya Bwana Mungu Mwenye vikosi, kwa kuwa wana wa Isiraeli wameliacha Agano lako, wakapabomoa pote pa kukutambikia, nao wafumbuaji wako wakawaua kwa panga, nikasalia mimi peke yangu; tena roho yangu nayo wanaitafuta, waichukue. Akaambiwa: Toka, usimame mlimani mbele ya Bwana, uone jinsi Bwana anavyopita! Pakaja upepo wenye nguvu nyingi ulioporomosha milima na kuvunja magenge, ukamtangulia Bwana, lakini Bwana hakuwamo mle upeponi. Upepo ulipokwisha pita, pakafuata mtetemeko wa nchi, lakini Bwana hakuwamo katika mtetemeko. Mtetemeko ulipokwisha pita, pakafuata moto, lakini namo motoni Bwana hakuwamo. Moto ulipokwisha pita, pakaja sauti nyembamba yenye upole. Elia alipoisikia, akaufunika uso wake kwa kanzu yake, akatoka kusimama langoni mwa pango; ndipo, aliposikia, sauti ikimwuliza: Unafanya nini humu, Elia? Akajibu: Nimejihimiza sana kwa ajili ya Bwana Mungu Mwenye vikosi, kwani wana wa Isiraeli wameliacha Agano lako, wakapabomoa pote pa kukutambikia, nao wafumbuaji wako wakawaua kwa panga, nikasalia mimi peke yangu; tena roho yangu nayo wanaitafuta, waichukue. Ndipo, Bwana alipomwambia: Nenda kuirudia hiyo njia ya nyikani, ufike Damasko! Utakapofika, umpake Hazaeli mafuta, awe mfalme wa Ushami. Naye Yehu, mwana wa Nimusi, umpake mafuta, awe mfalme wa Waisiraeli! Naye Elisa, mwana wa Safati, wa Abeli-Mehola umpake mafuta, awe mfumbuaji mahali pako! Itakuwa, atakayeukimbia upanga wa Hazaeli Yehu atamwua, naye atakayeukimbia upanga wa Yehu Elisa atamwua. Nami nitasaza katika Waisiraeli 7000, ndio wote wasiompigia Baali magoti, ndio wote wasiomnonea. Alipoondoka huko akamwona Elisa, mwana wa Safati, akilima na ng'ombe, jozi 12 zilikuwa mbele yake, naye alikuwa pale penye ile ya kumi na mbili; Elia akamwendea, akamtupia kanzu yake. Ndipo, alipowaacha ng'ombe wake, akamkimbilia Elia, akamwambia: Nipe ruhusa, kwanza ninoneane na baba na mama! Kisha nitakufuata. Akajibu: Nenda, uridi upesi! Usisahau niliyokutendea! Aliporudi, amfuate, akachukua ng'ombe wawili, akawaua; kisha akazipika nyama zao na kuvitumia vyombo vya hao ng'ombe kuwa kuni; hizo nyama zao akawagawia watu wake, wazile. Kisha akaondoka, akamfuata Elia na kumtumikia. Benihadadi, mfalme wa Ushami, akavikusanya vikosi vyake vyote, hata wafalme 32 walikuwa naye pamoja na farasi na magari, akaja kuusonga Samaria kwa kuuzinga, apigane nao. Akatuma wajumbe kwenda mjini kwa Ahabu, mfalme wa Waisiraeli. akamwambia: Ndivyo, Benihadadi anavyosema: Fedha zako na dhahabu zako ni zangu, na wake zako na watoto wako walio wazuri ni wangu. Mfalme wa Waisiraeli akajibu kwamba: Na yawe, kama ulivyosema, bwana wangu mfalme! Mimi ni mtu wako, navyo vyote, nilivyo navyo, ni vyako. Wajumbe wakarudi tena, wakasema: Hivi ndivyo, Benihadadi anavyosema kwamba: Kweli nimetuma kwako kukuambia: Fedha zako na dhahabu zako na wake zako na watoto wako utanipa. Lakini kesho saa hizi nitatuma watumishi wangu kwako, waichunguze nyumba yako, nazo nyumba za watumishi wako, wakamate kwa mikono yao yote yanayokupendeza, wayachukue. Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipowaita wazee wote wa nchi, akawaambia: Jueni, mwone, ya kuwa huyu anatafuta mabaya. Kwani alipotuma kwangu kuwataka wake zangu na watoto wangu na fedha zangu na dhahabu zangu, sikumnyima. Wazee wote na watu wote wakamwambia: Usimwitikie, wala usikubali! Basi, akawaambia wajumbe wa Benihadadi: Mwambieni bwana wangu mfalme: Yote, uliyomtumia mtumishi wako hapo kwanza, nitayafanya; lakini neno hili siwezi kulifanya. Wajumbe wakaenda zao kumpelekea hili jibu. Benihadadi akatuma kwake kumwambia: Mungu anifanyizie hivi, tena hivi, kama mavumbi ya Samaria yatatosha kuyajaza magao ya watu wote waliozifuata nyayo zangu! Mfalme wa Waisiraeli akajibu akisema: Mwambieni: Mwenye kujifunga mata asijivune akiwa hajayavua! Naye alipolisikia neno hili, alikuwa akinywa na wafalme wenziwe mabandani, akawaambia watumishi wake: Haya! Jipangeni! Wakajipanga, waujie huo mji. Mara mfumbuaji mmoja akafika kwa Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kumbe umeuona huo mtutumo mkubwa wote wa watu? Utaona leo, nikiwatia mkononi mwako, upate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana. Ahabu akauliza: Kwa msaada wa nani? Akasema: Hivi ndivyo, Bwana anvyosema: Kwa msaada wa vijana wa wakuu wa majimbo. Akauliza tena: Ni nani atakayeanza kupigana? akajibu: Wewe. Kwa hiyo akawakagua vijana wa wakuu wa majimbo, wakawa 232; kisha akawakagua watu wote wa wana wa Isiraeli, wakawa 7000. Wakatoka mnamo saa sita, Benihadadi alipokuwa anakunywa na kulewa mabandani pamoja na wale wafalme wenziwe 32 waliomsaidia. Wale vijana wa wakuu wa majimbo walipoanza kutoka, wote, Benihadadi aliowatuma, wakampasha habari kwamba: Watu wanatoka Samaria. Akasema: Kama wanatokea mapatano, wakamateni, wa hai! Kama wanatokea mapigano, vilevile wakamateni, wa hai! Lakini hao vijana wa wakuu wa majimbo walipokwisha kutoka mjini pamoja na vikosi vilivyowafuata, wakaua kila mtu wake wa kukutana naye; ndipo, Washami walipokimbia, nao Waisiraeli wakawakimbiza, lakini Benihadadi, mfalme wa Washami, akapona kwa farasi pamoja na wengine waliopanda farasi. Kisha naye mfalme wa Waisiraeli akatoka, akapiga farasi na magari, akawapiga Washami, wakauawa wengi mno. Kisha yule mfumbuaji akamtokea mfalme wa Waisiraeli, akamwambia: Nenda, ujipatie nguvu! Kwa hayo, uliyoyaona, ujue ya kufanya! Kwani mwaka utakapopita, mfalme wa Ushami atapanda tena, akujie. Watumishi wa mfalme wa Ushami wakamwambia: Mungu wa milima ni Mungu wao, kwa sababu hii wametushinda. Lakini tungepigana nao katika nchi ya tambarare, tungewashinda. Fanya hivi tu: waondoe wafalme kila mmoja mahali pake, uweke watawala nchi mahali pao! Kisha jihesabie vikosi, kama vile vilivyokuwa ulivyofiwa navyo, tena farasi kwa farasi, na gari kwa gari, tupigane nao katika nchi ya tambarare, tuone, kama sisi hatutawashinda. Basi, akayaitikia, waliyomwambia, akafanya hivyo. Mwaka ulipopita, Benihadadi akawakagua Washami, akawapeleka Afeki kupigana na Waisiraeli. Nao wana wa Isiraeli walipokwisha kukaguliwa na kupewa posho wakatoka kuja kukutana nao, wakapiga makambi nyuma yao, wakawa kama vikundi viwili vya mbuzi, nao Washami walikuwa wameieneza hiyo nchi. Ndipo, yule mtu wa Mungu alipofika kwake mfalme wa Waisiraeli, akasema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa kuwa Washami wamesema: Bwana ni Mungu wa milima, lakini siye Mungu wa mabonde, basi, huu mtutumo mkubwa wote wa watu nitautia mkononi mwako, mpate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana. Hivyo wakakaa makambini na kuelekeana siku saba; siku ya saba wakakaribiana kupigana. Ndipo, wana wa Isiraeli walipowaua hiyo siku moja Washami 100000 waendao kwa miguu. Waliosalia wakaukimbilia mji wa Afeki, boma la mji likawaangukia wale watu 27000 waliokuwa wamesalia, naye Benihadadi aliukimbilia huo mji na kuingia chumba kwa chumba. Kisha watumishi wake wakamwambia: Tazama, tumesikia, ya kuwa wafalme wa mlango wa Isiraeli ndio wafalme wenye upole; na tuvae magunia viunoni petu na kamba vichwani petu, kisha tumtokee mfalme wa Waisiraeli, hivyo labda atakuacha, ukae. Wakajifunga magunia viunoni pao na kamba vichwani pao, wakaja kwa mfalme wa Waisiraeli, wakasema: Mtumishi wako Benihadadi anaomba: Niache, nikae! Akauliza: Kumbe yuko mzima bado? Ni ndugu yangu! Neno hili wale watu wakaliwazia kuwa si ndege mbaya, wakajihimiza kutambua, kama ndilo lililomo moyoni mwake kweli, wakauliza: Benihadadi ni ndugu yako kweli? Akajibu: Nendeni kumchukua! Ndipo, Benihadadi alipomtokea, naye akampandisha garini. Benihadadi akamwambia: Miji, baba yangu aliyoichukua kwa baba yako, nairudisha; tena utajipatia njia za kuingia Damasko, kama baba yangu alivyojipatia njia ya kuingia Samaria. (Ahabu akasema): Kwa agano hili nitakuacha, ujiendee. Basi, akafanya agano naye, kisha akamwacha, ajiendee. Kisha mmoja wao wanafunzi wa wafumbuaji akamwambia mwenziwe kwa kuagizwa na Bwana: Unipige! Yule mwenziwe akakataa kumpiga. Naye akamwambia: Kwa kuwa hukuiitikia sauti ya Bwana, ukitoka kwangu, utaona simba, naye atakuua! Basi alipotoka kwake, simba akamwona, akamwua. Alipoona mtu mwingine akamwambia: Nipige! Yule mtu akampiga sana na kumtia kidonda. Kisha huyu mfumbuaji akaja kusimama njiani, mfalme alipotaka kupitia, lakini alikuwa amejigeuza, asijulikane, kwa kufunga kitambaa machoni pake. Ikawa, mfalme alipopita, yeye akamlilia mfalme akisema: Mtumishi wako alikuwa amekwenda penye yale mapigano; mara mwenzangu aliyekuwa ameondoka akaniletea mtu, akaniambia: Mwangalie mtu huyu! Atakapopotea, mwenyewe utaingia mahali pake au utajikomboa kwa kulipa kipande cha fedha, ndio shilingi 12000. Basi, mtumishi wako alipokuwa anafanya hivi na hivi, mara yule mtu alikuwa hayuko. Mfalme wa Waisiraeli akamwambia: Basi, shauri lako ni lilelile, ulilojikatia mwenyewe! Ndipo, alipokiondoa upesi kile kitambaa machoni pake, naye mfalme wa Waisiraeli akamtambua, ya kuwa ni mmoja wao wafumbuaji. Naye akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtu, mimi niliyemtoa, aangamizwe, wewe umemwacha, aponyoke mikononi mwako, kwa sababu hii roho yako itakuwa mahali pake, nao wa ukoo wako watakuwa mahali pao wa ukoo wake. Kisha mfalme wa Waisiraeli akaenda nyumbani kwake mwenye moyo uliokasirika na kuchafuka, akafika Samaria. Hayo yalipokwisha kufanyika, kulikuwa na mtu wa Izireeli, ndiye Naboti; alikuwa na shamba la mizabibu huko Izireeli karibu ya jumba la Ahabu, mfalme wa Samaria. Ahabu akamwambia Naboti: Nipe shamba lako la mizabibu, liwe langu, nipapande mboga! Kwani ni karibu ya nyumba yangu. Nami mahali pake nitakupa shamba la mizabibu lililo zuri zaidi, au kama unapendezwa, nitakupa fedha kuwa malipo yake. Naboti akamwambia Ahabu: Bwana na anizuie, nisikupe fungu langu, nililolipata kwa baba zangu! Ahabu akaenda nyumbani mwake mwenye moyo uliokasirika na kuchafuka kwa ajili ya hilo neno, Naboti wa Izireeli alilomwambia kwamba: Sitakupa fungu langu, nililolipata kwa baba zangu. Akaja kulala kitandani pake, akauelekeza uso ukutani, akakataa kula chakula. Ndipo, mkewe Izebeli alipoingia mwake, akamwambia: Mbona roho yako inakasirika, ukakataa kula? Akamwambia: Nimesema na Naboti wa Izireeli, nikamwambia: Nipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au kama unapendezwa, nitakupa shamba jingine la mizabibu mahali pake; naye akajibu: Sitakupa shamba langu la mizabibu. Mkewe Izebeli akamwambia: Sasa wewe sharti uonyeshe, ya kuwa ndiwe mfalme wa Waisiraeli; inuka, ule, nao moyo wako na utulie! Mimi nitakupa shamba la mizabibu la Naboti wa Izireeli. Akaandika barua katika jina la Ahabu, akaitia muhuri ya mfalme, akaituma hiyo barua kwa wazee na kwa wakuu wa mji waliokaa humo na Naboti. Akaandika humo baruani kwamba: Tangazeni mfungo, naye Naboti mwekeni kuwa mkuu wa watu! Kisha wekeni kila kando yake watu wawili wasiofaa, wapate kumsingizia kwamba: Amemtukana Mungu na mfalme. Kisha mtoeni mjini, mmpige mawe, afe! Wazee na wakuu waliokaa naye katika mji wake wakafanya hivyo, kama Izebeli alivyowatuma, kama vilivyoandikwa katika ile barua, aliyoituma kwao. Wakatangaza mfungo, wakamweka Naboti kuwa mkuu wa watu. Wakaja watu wawili wasiofaa kitu, wakakaa kando yake, kisha hao watu wasiofaa kitu wakamsingizia Naboti mbele ya watu kwamba: Naboti amemtukana Mungu na mfalme; kwa hiyo wakamtoa nje ya mji, wakampiga mawe, mpaka akifa. Kisha wakatuma kwake Izebeli kumwambia: Naboti amepigwa mawe, akafa. Izebeli aliposikia, ya kuwa Naboti amepigwa mawe, akafa, Izebeli akamwambia Ahabu: Haya! Litwae shamba la mizabibu la Naboti wa Izireeli, alilokataa kukupa kwa fedha! Kwani Naboti hayupo, kwani amekwisha kufa. Ikawa, Ahabu aliposikia, ya kuwa Naboti amekufa, Ahabu akaondoka kushuka kwenye shamba la mizabibu la Naboti wa Izireeli, aje kulitwaa. Kisha neno la Bwana likamjia Elia wa tisibe kwamba: Inuka, ushuke kumwendea Ahabu, mfalme wa Isiraeli, aliye huko Samaria! Utamwona katika shamba la mizabibu la Naboti, alikokwenda kulichukua. Umwambie kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kumbe umeua, kisha ukazitwaa mali za mfu? Kisha umwambie kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mahali pale, mbwa walipoilamba damu ya Naboti, palepale mbwa watailamba nayo damu yako wewe. Ndipo, Ahabu alipomwambia Elia: Je? Umeniona, wewe mchukivu wangu? Akajibu: Nimeona, ya kuwa umejiuza kuwa mtumwa wa mambo yaliyo mabaya machoni pa Bwana, uyafanye. Utaniona, nikikuletea mabaya, nikuzoe. Kweli nitawatowesha wa Ahabu walio wa kiume, kama watakuwa wamefungwa, au kama watakuwa wamefunguliwa kwao Waisiraeli. Nitautoa mlango wako kuwa kama mlango wa Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kama mlango wa Basa, mwana wa Ahia, kwa ajili ya hayo machafuko, uliyonichafukisha kwa kuwakosesha Waisiraeli. Kwa ajili yake Izebeli Bwana akasema kwamba: Mbwa watamla Izebeli katika mfereji wa mji wa Izireeli. Wao wa Ahabu watakaokufa mjini mbwa watawala; nao watakaokufa shambani madege wa angani watawala. Kweli hakuwako mtu kama Ahabu aliyejiuza hivyo kuwa mtumwa wa mambo yaliyo mabaya machoni pa Bwana, ayafanye; ni kwa kuwa mkewe Izebeli alimpoteza. Akatapisha sana kwa kuyafuata magogo ya kutambikia na kuyafanya yote, Waamori waliyoyafanya, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Isiraeli. Ikawa, Ahabu alipoyasikia hayo maneno akazirarua nguo zake, akajivika gunia mwilini pake, akafunga mfungo; hata kulala akalala na kuvaa gunia, akawa akijiendeaendea na kunyamaza kimya. Ndipo, neno la Bwana lilipomjia Elia wa Tisibe kwamba: Umeona, ya kuwa Ahabu amejinyenyekeza machoni pangu? Kwa kuwa amejinyenyekeza machoni pangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake, lakini katika siku za mwanawe nitauletea mlango wake yale mabaya. Wakakaa miaka mitatu, Washami na Waisiraeli wasipopigana. Ikawa katika mwaka wa tatu, akashuka Yosafati, mfalme wa Wayuda, kuja kwake mfalme wa Waisiraeli. Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipowaambia watumishi wake: Je? Mwajua, ya kuwa Ramoti wa Gileadi ni wa kwetu? Nasi tunajikalia tu tukiacha kuuchukua mkononi mwa mfalme wa Washami? Alipomwuliza Yosafati: Utakwenda pamoja na mimi Ramoti wa Gileadi kupiga vita? Yosafati akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, nao farasi wangu ni kama farasi wako. Kisha Yosafati akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Uliza leo hivi, Bwana atakavyosema! Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipowakusanya wafumbuaji, watu 400, akawauliza: Niende Ramoti wa Gileadi kupiga vita, au niache? Wakasema: Panda tu! Bwana atautia mkononi mwa mfalme. Yosafati akauliza: Huku hakuna tena mfumbuaji wa Bwana, tumwulize naye? Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: Yuko bado mtu mmoja wa kumwuliza neno la Bwana, lakini mimi ninamchukia, kwani hanifumbulii mema, ila mabaya tu, ndiye Mikaya, mwana wa Imula. Yosafati akasema: Mfalme asiseme hivyo! Ndipo, mfalme alipomwita mtumishi mmoja wa nyumbani, akamwambia: Piga mbio kumwita Mikaya, mwana wa Imula! Mfalme wa Waisiraeli na Yosafati, mfalme wa Wayuda, walikuwa wamekaa kila mmoja katika kiti chake cha kifalme na kuvaa mavazi, wakawa wakikaa hapo pa kupuria ngano penya lango la kuuingilia mji wa Samaria, nao wafumbuaji wote wakawa wakifumbua mbele yao. Ndipo, Sedekia, mwana wa Kenaana, alipojifanyizia pembe za chuma, akasema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa pembe kama hizi utawakumba Washami, mpaka uwamalize. Nao wafumbuaji wote wakafumbua hivyo kwamba: Upandie Ramoti wa Gileadi! Utafanikiwa, naye Bwana atautia mkononi mwake mfalme! Yule mjumbe aliyekwenda kumwita Mikaya akamwambia kwamba: Tazama, maneno ya wafumbuaji ni kinywa kimoja tu cha kufumbua mema yatakayomjia mfalme. Basi, neno lako nalo na liwe kama neno la mmoja wao hao, useme mema yatakayokuwa. Mikaya akasema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, nitasema hayo tu, Bwana atakayoniambia. Alipofika kwake mfalme, mfalme akamwuliza: Mikaya, twende Ramoti wa Gileadi kupiga vita, au tuache? Akamwambia: Upandie tu! Utafanikiwa, naye Bwana atautia mkononi mwake mfalme. Mfalme akamwambia: Nimekuapisha mara nyingi, usiniambie mengine katika Jina la Bwana, isipokuwa iliyo ya kweli. Ndipo, aliposema: Nimewaona Waisiraeli, nao walikuwa wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Bwana akasema: Hawa hawana bwana, na warudi na kutengemana kila mtu nyumbani kwake. Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: Sikukuambia: Hanifumbulii yatakayokuwa mema, ila yatakayokuwa mabaya tu? Mikaya akasema: Lakini lisikie neno la Bwana! Nimemwona Bwana, akikaa katika kiti chake kitukufu, navyo vikosi vyote vya mbinguni vilisimama mbele yake, kuumeni na kushotoni kwake. Bwana akauliza: Yuko nani atakayemponza Ahabu, aje kuupandia Ramoti wa Gileadi, aangushwe huko? Wakajibu, mmoja akisema hivi, mmoja hivi. Kisha akatokea roho, akasimama mbele ya Bwana, akasema: Mimi nitamponza. Bwana akamwuliza: Kwa nini? Akasema: Nitatoka kuwa roho ya uwongo vinywani mwa wafumbuaji wake wote. Bwana akasema: Utamponza kweli, utaweza hivyo, toka kufanya hivyo! Sasa tazama! Bwana ametia roho ya uwongo vinywani mwa hawa wafumbuaji wako wote, maana yeye Bwana amekwisha kukutakia mabaya. Ndipo, Sedekia, mwana wa Kenaana, alipomkaribia Mikaya, akampiga makofi na kumwuliza: Roho ya Mungu imeshika njia gani, inipite mimi, ije kusema na wewe? Mikaya akasema: Jiangalie! Utaviona siku hiyo, utakapoingia chumba kwa chumba, upate kujificha. Mfalme wa Waisiraeli akasema: Mchukue Mikaya, mrudishe kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoasi, mwana wa mfalme, useme: Hivi ndivyo, mfalme anavyosema: Mwekeni huyu kifungoni, mmpe chakula cha mahangaiko na maji ya mahangaiko, hata nitakapofika salama. Mikaya akasema: Kama utarudi salama, Bwana hakusema kinywani mwangu. Kisha akasema: Lisikieni hili, ninyi makabila yote! Kisha mfalme wa Waisiraeli na Yosafati, mfalme wa Wayuda, wakaupandia Ramoti wa Gileadi. Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: Nitavaa nguo nyingine, niingie penye mapigano, lakini wewe zivae nguo zako! Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipovaa nguo nyingine, kisha akafika penye mapigano. Naye mfalme wa Ushami alikuwa amewaagiza wakuu wake wa magari 32 kwamba: Msipigane na mtu ye yote, mdogo kwa mkubwa, ila mpigane na mfalme wa Waisiraeli peke yake tu! Ikawa, wakuu wa magari walipomwona Yosafati wakamwazia yeye kuwa mfalme wa Waisiraeli, wakamgeukia kupigana naye; ndipo, Yosafati alipopiga yowe. Ikawa, wakuu wa magari walipoona, ya kuwa siye mfalme wa Waisiraeli, wakarudi na kuacha kumfuata. Kulikuwa na mtu, akauvuta upindi wake kwa kubahatisha tu, akampiga mfalme wa Waisiraeli hapo, vyuma vya kisibau chake vilipounganishwa. Ndipo, alipomwambia mwendeshaji wake wa gari: Ligeuze kwa mkono wako, unitoe hapa, wanapopigana, kwani nimeumia. Mapigano yakazidi siku hiyo; kwa hiyo mfalme alikuwa amesimama garini ng'ambo ya huku ya Washami, akafa jioni; nayo damu ya kidonda chake ilikuwa imemwagika ndani ya gari. Jua lilipokuchwa, mbiu ikapigwa makambini kwamba: kila mtu na arudi mjini kwake! Kila mtu na arudi katika nchi yake! Mfalme alipokwisha kufa, akapelekwa Samaria; ndiko, walikomzika mfalme wa Samaria. Walipolisafisha lile gari kwa maji penye ziwa la Samaria, mbwa wakailamba damu yake nao wanawake wagoni wakaoga papo hapo, kama Bwana alivyosema. Mambo mengine ya Ahabu nayo yote, aliyoyafanya, na habari za ile nyumba ya pembe za tembo, aliyoijenga, nazo za miji yote, aliyoijenga, hazikuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Ahabu alipokwisha kulala na baba zake, mwanawe Ahazia akawa mfalme mahali pake. Yosafati, mwana wa Asa, akapata kuwa mfalme wa Wayuda katika mwaka wa 4 wa Ahabu, mfalme wa Waisiraeli. Yosafati alikuwa mwenye miaka 35 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 25; jina la mama yake ni Azuba, binti Silihi. Akaendelea kuzishika njia zote za baba yake Asa, hakuziacha kabisa, akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana. Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, watu wakaendelea bado kutoa huko ng'ombe za tambiko na kuvukiza kule vilimani. Yosafati akakaa na kupatana na mfalme wa Waisiraeli. Mambo mengine ya Yosafati na matendo yake yenye nguvu, aliyoyafanya alipopiga vita, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Nao wagoni wa patakatifu waliosalia katika siku za baba yake Asa akawatowesha kabisa katika hiyo nchi. Kule Edomu siku zile hakuwako mfalme mwenyewe ni mtawala nchi tu aliyeshika ufalme. Yosafati akajitengenezea merikebu za Tarsisi kwenda Ofiri kuchukua dhahabu, lakini hazikufika, kwani hizo merikebu za Tarsisi zilivunjika Esioni-Geberi. Siku zile Ahazia, mwana wa Ahabu, alimwambia Yosafati: Watumishi wangu, na waende pamoja na watumishi wako merikebuni. Lakini Yosafati akakataa. Yosafati akaja kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa baba yake Dawidi, naye mwanawe Yoramu akawa mfalme mahali pake. Ahazia, mwana wa Ahabu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli kule Samaria katika mwaka wa 17 wa Yosafati, mfalme wa Wayuda, akawa mfalme wa Waisiraeli miaka 2. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, akaendelea kuishika njia ya baba yake na njia ya mama yake na njia ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli. Akamtumikia Baali na kumtambikia, akamchafukisha Bwana Mungu wa Isiraeli kwa kuyafanya yote, baba yake aliyoyafanya. Ahabu alipokwisha kufa, Wamoabu wakawavunjia Waisiraeli maagano. Ahazia akaanguka dirishani penye chumba chake cha juu mle Samaria, akapata kuugua; ndipo, alipotuma wajumbe, aliowaambia: Nendeni kumwuliza Baali-Zebubu, mungu wa Ekroni, kama nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Elia wa Tisibe: Inuka, uwaendee wajumbe wa mfalme wa Samaria, uwaambie: Je? Kwao Waisiraeli hakuna Mungu, ninyi mkienda kumwuliza Baali-Zebubu, mungu wa Ekroni? Kwa sababu hii Bwana anasema: Hutaondoka tena hapo kitandani, unapolala, ila utakufa kweli, Kisha Elia akaenda zake. Wajumbe waliporudi kwake mfalme, akawauliza: Mbona mnarudi? Wakamwambia: Mtu ametujia, akatuambia: Haya! Rudini kwa mfalme aliyewatuma, mmwambie: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Je? Kwao Waisiraeli hakuna Mungu, wewe ukituma kumwuliza Baali-Zebubu, mungu wa Ekroni? Kwa sababu hii hutaondoka tena hapo kitandani, unapolala, ila utakufa kweli. Akawauliza: Yule mtu aliyewajia na kuwaambia maneno hayo alikuwa na sura gani? Wakamwambia: Yule mtu alikuwa amevaa ngozi yenye manyoya, aliyoifunga kwa ukanda wa ngozi viunoni pake. Ndipo, aliposema: Ndiye Elia wa Tisibe. Kisha mfalme akatuma kwake Elia mkuu wa kikosi cha hamsini pamoja na watu wake hamsini; alipopanda huko, aliko, akamwona, akikaa juu mlimani, akamwambia: Mtu wa Mungu, mfalme anakuagiza: Shuka! Lakini Elia akamjibu huyu mkuu wa hamsini na kumwambia: Kama mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke toka mbinguni, ukule wewe na watu wako hamsini. Akatuma tena kwake mkuu mwingine wa kikosi cha hamsini na watu wake hamsini, naye akasema na kumwambia: Mtu wa Mungu, ndivyo, mfalme anavyosema: Shuka upesi! Elia akawajibu kwamba: Kama mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke toka mbinguni, ukule wewe na watu wako hamsini. Ndipo, moto uliposhuka toka mbinguni, ukamla na watu wake hamsini. Akatuma mara ya tatu mkuu wa kikosi cha hamsini na watu wake hamsini; huyu mkuu wa tatu wa kikosi cha hamsini alipopanda na kufika kwake akampigia Elia magoti, akamwambia na kumbembeleza: Mtu wa Mungu, roho yangu nazo roho za hawa watumishi wako hamsini usiziwazie kuwa si kitu! Tazama, moto ulishuka toka mbinguni, ukawala wale wakuu wa hamsini wawili wa kwanza na watu wao hamsini hamsini, sasa roho yangu usiiwazie kuwa si kutu! Ndipo, malaika wa Bwana alipomwambia Elia: Shuka naye, usimwogope! Basi, akaondoka, akashuka naye kwenda kwa mfalme. Akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa kuwa umetuma wajumbe kumwuliza Baali-Zebubu, mungu wa Ekroni, kama hakuna Mungu kwao Waisiraeli wa kumwuliza, atakavyosema, kwa sababu hii hutaondoka tena hapa kitandani, unapolala, ila utakufa kweli. Akafa, kwa hilo neno la Bwana, Elia alilolisema; kisha Yoramuakawa mfalme mahali pake katika mwaka wa pili wa Yoramu, mwana wa Yosafati, mfalme wa Wayuda, kwani Ahazia hakuwa na mwana. Mambo mengine ya Ahazia, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Bwana alipotaka kumpaza Elia mbinguni kwa nguvu za upepo wenye ngurumo, Elia na Elisa walikuwa wakienda njiani kutoka Gilgali. Elia akamwambia Elisa: Kaa hapa! Kwani Bwana amenituma kwenda Beteli. Elisa akajibu: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena hivyo, wewe mwenyewe ulivyo mzima, sitakuacha kabisa. Wakatelemka kwenda Beteli. Ndipo, wanafunzi wa wafumbuaji waliomo Beteli walipomtokea Elisa, wakamwambia: Unajua, ya kuwa leo Bwana atamwondoa bwana wako kichwani pako? Akasema: Nami nayajua, nyamazeni tu! Elia akamwambia: Elisa, kaa hapa! Kwani Bwana amenituma kwenda Yeriko. Akajibu: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena hivyo, wewe mwenyewe ulivyo mzima, sitakuacha kabisa. Wakaja Yeriko. Ndipo, wanafunzi wa wafumbuaji waliomo Yeriko walipomjia Elisa, wakamwambia: Unajua, ya kuwa leo Bwana atamwondoa bwana wako kichwani pako? Akasema: Nami nayajua, nyamazeni tu! Elia akamwambia: Kaa hapa! Kwani Bwana amenituma kwenda Yordani. Akajibu: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena hivyo, wewe mwenyewe ulivyo mzima, sitakuacha kabisa. Wakaenda wote wawili. Watu hamsini waliokuwa wanafunzi wa wafumbuaji wakaja, wakasimama mbali ng'ambo ya huku, wao wawili waliposimama Yordani. Ndipo, Elia alipolishika joho lake, akalizinga, akalipigisha maji; ndipo, yalipogawanyika huku na huko, nao wote wawili wakapita pakavu. Walipokwisha pita, Elia akamwambia Elisa: Omba unayoyataka, nikufanyizie, nikiwa sijaondolewa kwako! Elisa akasema: Ninataka, mafungu mawili ya roho yako yaje kunikalia. Elia akajibu: Umeomba neno gumu. Utakaponiona, nikiondolewa kwako, na ulipate! Usipoviona, hutalipata. Ikawa, wangaliko njiani na kusema, mara gari la moto likatokea pamoja na farasi wa moto, likawatenga wale wawili. Ndivyo, Elia alivyopaa mbinguni kwa nguvu za upepo wenye ngurumo. Elisa alipoviona akalia kwamba: Baba yangu! Baba yangu! Wewe gari la Waisiraeli na wapanda farasi wake! Lakini hakumwona tena; kisha akazishika nguo zake, akazirarua, zitoke vipande viwili. Kisha akaliokota joho lake Elia lililokuwa limeanguka, akarudi, akasimama kando ya mto wa Yordani. Akalishika hilo joho la Elia lililokuwa limeanguka, akalipigisha maji akisema: Bwana Mungu wa Elia yuko wapi? Basi; hapo, yeye naye alipoyapiga maji, mara maji yakagawanyika huku na huko, naye Elisa akapita. Wanafunzi wa wafumbuaji waliokuwako Yeriko ng'ambo ya huku walipomwona wakasema: Roho yake Elia inamkalia Elisa. Wakamwendea, wakamwangukia chini. Wakamwambia: Tazama, huku wako watu hamsini wenye nguvu; acha, tuwatume, waende kumtafuta bwana wako! Labda roho ya Bwana imemchukua, ikamweka juu ya mlima mmoja au katika bonde moja. Akawaambia: Msiwatume! Walipomhimiza sana, mpaka akilegea, akasema: watumeni! Ndipo, walipowatuma wale watu hamsini, wakamtafuta siku tatu, lakini hawakumwona. Waliporudi kwake, yeye alikuwa angaliko Yeriko, akawaambia: Sikuwaambia, msiende? Kisha watu wa huo mji wakamwambia Elisa: Tazama, hapa, mji huu unapokaa, ni pema, kama wewe bwana unavyoona, lakini maji ni mabaya, kwa hiyo nchi hii hupoozesha mimba, ziharibike. Akasema: Nileteeni bakuli jipya, kisha tieni chumvi humo! Walipomletea, akaenda nje kufika hapo, maji yalipotokea, akaitupa ile chumvi papo hapo akisema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nimeyapatia maji haya uzima, hayataua tena, wala hayatapoozesha tena mimba. Ndipo, yale maji yalipopona hata siku hii ya leo, kama Elisa alivyosema. Toka huko akapanda kwenda Beteli; alipokuwa akipanda njiani, watoto wakatoka mjini, wakamfyoza wakimwambia: Panda, Chakipara! Panda, Chakipara! Alipogeuka nyuma akawaona, akawaapiza katika Jina la Bwana. Ndipo, chui wawili walipotoka mwituni, wakararua kwao watoto 42. Kisha akatoka huko kwenda mlimani kwa Karmeli, toka huko akarudi Samaria. Yoramu, mwana wa Ahabu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli huko Samaria katika mwaka wa 18 wa Yosafati, mfalme wa Wayuda, akawa mfalme miaka 12. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, lakini hakuzidi kama baba yake na mama yake, akaiondoa nguzo ya mawe ya kumtambikia Baali, baba yake aliyoitengeneza. Lakini makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli, aligandamana nayo, hakuyaacha. Mesa, mfalme wa Wamoabu, aliyekuwa mfuga kondoo alikuwa akimletea mfalme wa Waisiraeli wana kondoo 100000 na manyoya ya madume ya kondoo 100000. Lakini Ahabu alipokufa, mfalme wa Wamoabu akamvunjia mfalme wa Waisiraeli hayo maagano. Siku hiyo mfalme Yoramu akatoka Samaria kuwakagua Waisiraeli wote. Kisha akatuma kwa Yosafati, mfalme wa Wayuda, kumwuliza hivyo: Mfalme wa Wamoabu amenivunjia maagano; utakwenda pamoja na mimi vitani kupigana na Wamoabu? Akasema: Nitapanda kwenda huko; mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, nao farasi wangu ni kama farasi wako. Alipouliza: Tupande na kushika njia ipi? akasema: Njia ya nyika ya Edomu. Basi, wakaenda mfalme wa Waisiraeli na mfalme wa Wayuda na mfalme wa Waedomu. Walipokwenda na kuzunguka njia ya siku saba, walikuwa hawana maji ya vikosi vya makambini wala ya nyama waliozifuata nyayo zao. Ndipo, mfalme wa Waisiraeli aliposema: Yoi! Bwana amewaita hawa wafalme watatu, awatie mikononi mwa Wamoabu! Yosafati akauliza: Je? Hakuna mfumbuaji wa Bwana wa kumwuliza Bwana, yatakayokuwa? Ndipo, mmoja wao watumishi wa mfalme wa Waisiraeli akajibu: Yuko Elisa, mwana wa safati, aliyemmiminia Elia maji mikononi pake. Yosafati akasema: Kwake yeye neno la Bwana liko. Ndipo, mfalme wa Waisiraeli na Yosafati na mfalme wa Waedomu waliposhuka kuja kwake. Elisa akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Tuna bia gani mimi na wewe? Nenda kwa wafumbuaji wa baba yako na kwa wafumbuaji wa mama yako! Mfalme wa Waisiraeli akamwambia: La! Kweli Bwana amewaita hawa wafalme, awatie mikononi mwa Wamoabu. Elisa akasema: Hivyo, Bwana Mwenye vikosi alivyo Mwenye uzima, ambaye ninasimama mbele yake, kama nisingeutazama uso wa Yosafati, mfalme wa Wayuda, wewe nisingekuelekezea macho, nisikuone! Sasa nileteeni mpiga zeze! Ikawa, huyu mpiga zeze alipolipiga zeze lake, mara mkono wa Bwana ukamjia, akasema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Chimbeni humu bondeni mashimo po pote! Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: hamtaona upepo, wala hamtaona mvua, lakini bonde hili litajazwa maji, mpate kunywa ninyi nao mlio nao na nyama wenu. Nayo haya ni mepesi machoni pake Bwana, maana nao wamoabu atawatia mikononi mwenu. Ninyi mtaiteka miji yote yenye maboma na miji yote iliyochaguliwa. Mtaikata miti mizuri yote, navyo visima vyote vya maji mtavifukia na mashamba mazuri yote mtayaharibu kwa kuyatupia mawe. Ikawa asubuhi, walipotolea vipaji vya tambiko, ndipo, walipoona, maji yakija katika njia ya kutoka Edomu, mara nchi hiyo ikajaa maji. Wamoabu wote waliposikia, ya kuwa hao wafalme wanawapandia kupigana nao, wakakusanywa wote walioweza kujivika mata nao walio wazee, wakajipanga kuusimamia mpaka. Wakaamka na mapema, jua lilipochomoza juu ya yale maji; ndipo, Wamoabu walipoyaona yale maji mbele yao kuwa mekundu kama damu. Wakasema: Ni damu hizo; kumbe hao wafalme wamekosana, wakauana kila mtu na mwenzake. Sasa ninyi Wamoabu, haya! Chukueni nyara! Walipofika kwenye makambi ya Waisiraeli, Waisiraeli wakawaondokea, wakawapiga Wamoabu, nao wakawakimbia, kisha wakaendelea kuingia kwao wakiwapiga Wamoabu. Wakaibomoa miji, tena penye mashamba mazuri wakayatupia kila mtu jiwe lake, hivyo wakayajaza mawe, navyo visima vyote vya maji wakavifukia, hata miti mizuri yote wakaikata, hawakusaza mji, ni boma la mawe la Kiri-Hareseti peke yake tu. Huu nao wapiga makombeo wakauzunguka, waupige. Mfalme wa Wamoabu alipoona, ya kuwa mapigano hayo yatamshinda, asiyaweze, akachukua watu 700, kila mmoja akiuchomoa upanga wake, wajivunjie njia ya kwenda kwa mfalme wa Waedomu, lakini hawakuweza. Ndipo, alipomchukua mwanawe wa kwanza aliyetaka kumpokea ufalme, mwenyewe atakapokufa, akamtumia kuwa ng'ombe ya tambiko, akamteketeza ukutani juu. Ndipo, machafuko makubwa yalipowainukia Waisiraeli, wakaondoka huko, wakarudi kwao katika nchi yao. Kulikuwa na mwanamke wa wanafunzi wa wafumbuaji, akamlilia Elisa kwamba: Mume wangu, mtumishi wako, amekufa, nawe unajua, ya kuwa mtumishi wako alikuwa mwenye kumcha Bwana; tena mtu, aliyemkopa, amekuja kuwachukua wanangu mawili, wawe watumwa wake. Elisa akamwuliza: Nikufanyizie nini? Niambie, nyumbani mwako unavyo vyombo gani? Akajibu: Kijakazi wako hanacho cho chote nyumbani, ni kitungi cha mafuta tu. Akamwambia: Nenda kujiombea vyombo vitupu huko nje kwao wote walio majirani zako, lakini usichukue vichache! Kisha ingia mwako, ukaufunge mlango nyuma yako na nyuma ya wanao! Kisha yale mafuta yako uyatie katika hivyo vyombo vyote; kimoja kikijaa, kiweke! Akaondoka kwake, akaja kuufunga mlango nyuma yake na nyuma ya wanawe; nao wakamletea vyombo, naye akavitia mafuta. Vyombo vilipojaa, akamwambia mwanawe: Niletee chombo kingine. Akamwambia: Hakuna tena chombo kingine. Ndipo, yale mafuta yalipokoma. Basi, akaenda kumsimulia yule mtu wa Mungu yaliyokuwa, naye akamwambia: Nenda, uyauze hayo mafuta, umlipe yule anayekudai! Yatakayosalia yatumie wewe na wanao! Ikawa siku moja, Elisa akaenda Sunemu. Huko kulikuwa na mwanamke mkuu; huyu akakaza kumwomba, ale chakula kwake. Kwa hiyo kila mara alipopita hapo akafikia kwake kula chakula. Kisha yule mwanamke akamwambia mumewe: Tazama, nimetambua, ya kuwa yule mtu asiyekawa kufikia kwetu ni mtu mtakatifu wa Mungu. Na tumtengenezee darini chumba kidogo, tukaweke mle kitanda na meza na kiti na taa, kila atakapokuja kwetu afikie mlemle. Ikawa siku nyingine, alipokuja huko akafikia mle chumbani, akalala humo. Akamwambia mtoto wake Gehazi: Mwite huyo mwanamke wa Sunemu! Akamwita, naye akaja kusimama mbele yake. Akamwambia Gehazi: Mwambie: Nimeona, ulivyotusumbukia hayo masumbuko yote; nami nikufanyie nini? Unalo neno la kukusemea kwa mfalme au kwa mkuu wa vikosi? Akajibu: Mimi ninajikalia katikati yao walio ukoo wangu. Alipouliza tena: Nimfanyie nini? Gehazi akajibu: Hana mtoto. Naye mumewe ni mzee. Akasema: Mwite! Alipomwita, akaja, akasimama mlangoni. Akamwambia: Mwaka utakapopita, wakati kama huu utabeba mwana wa kiume kifuani. Akajibu: Bwana wangu, u mtu wa Mungu, uwimwongopee kijakazi wako! Lakini yule mwanamke akapata mimba, nao mwaka ulipopita, wakati huohuo akazaa mwana wa kiume, kama Elisa alivyomwambia. Mtoto alipokua, siku moja akatoka kwenda kwa baba yake shambani kwenye wavunaji. Mara akamwambia baba yake: Kichwa changu! Kichwa changu! Ndipo, alipomwambia kijana: Mpeleke kwa mama yake! Akamchukua, akampeleka kwa mama yake, akakaa magotini kwake mpaka saa sita; ndipo, alipokufa. Akampeleka juu, akamlaza kitandani pake yule mtu wa Mungu, akafunga mlango nyuma yake, akatoka. Kisha akamwita mumewe, akamwambia: Tuma kwangu kijana mmoja na punda jike moja, nipige mbio kwenda kwake yule mtu wa Mungu, kisha nirudi! Akamwuliza: Sababu gani unataka kwenda kwake leo hivi? Hakuna mwandamo wa mwezi wala siku ya mapumziko. Akajibu: Si neno. Kisha akamtandika punda, akamwambia kijana wake: Uende ukimkimbiza, usinikawilishe safarini, nisipokuambia! Ndivyo, alivyokwenda, akafika kwa yule mtu wa Mungu mlimani kwa Karmeli. Yule mtu wa Mungu alipomwona ng'ambo ya huko akamwambia mtoto wake Gehazi: Tazama, yule kule ni mwanamke wa Sunemu! Sasa piga mbio, umkute njiani, umwulize: Hujambo? Naye mumeo hajambo? Naye mtoto hajambo? Akajibu: Hawajambo. Alipofika mlimani kwake yule mtu wa Mungu akamshika miguu; ndipo, Gehazi alipokuja, amwondoe, lakini yule mtu wa Mungu akamwambia: Mwache! Kwani anayo machungu rohoni; naye Bwana amenificha jambo hili, hakuniambia. Ndipo, yule mwanamke aliposema: Bwana wangu, nilikuomba kunipatia mtoto? Sikukuambia: Usinidanganye? Naye Elisa akamwambia Gehazi: Funga viuno vyako, uichukue fimbo yangu mkononi mwako, uende! Ukiona mtu, usimwamkie! Kama anakuamkia, usimjibu! Uiweke fimbo yangu usoni pa mtoto! Ndipo, mama ya mtoto aliposema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena hivyo, wewe mwenyewe ulivyo mzima, sitakuacha kabisa! Ndipo, alipoinuka kufuatana naye. Lakini Gehazi alikuwa amekwenda mbele yao, akaiweka ile fimbo usoni pa mtoto, lakini haikuwako sauti wala pumzi. Ndipo, aliporudi kukutana naye mwenyewe, akamwambia kwamba: Mtoto hakuamka. Elisa alipoingia mle chumbani akamwona mtoto, ya kuwa ni mfu, amelazwa kitandani pake. Akaenda, akajifungia mlango, wawe wawili tu, yeye na mtoto, kisha akamwomba Bwana. Akapanda, akamlalia mtoto akiweka kinywa chake kinywani pake na macho yake machoni pake navyo viganja vyake viganjani pake; alipomlalia hivyo, mwili wake mtoto ukapata jasho. Kisha Elisa akaondoka tena, akatembea chumbani mara moja huku, mara moja huko, kisha akapanda tena kumlalia hivyo; ndipo, mtoto alipopiga chafya mara saba, kisha akayafumbua macho yake. Akamwita Gehazi, akamwambia: Mwite huyo mwanamke wa Sunemu! Akamwita. Alipoingia kwake, akamwambia: Mchukue mwanao! Akaja, akamwangukia miguuni pake na kumwinamia; kisha akamchukua mwanawe, akatoka. Elisa aliporudi Gilgali, kulikuwa na njaa katika nchi hiyo. Wanafunzi wa wafumbuaji walipokuja kukaa mbele yake, akamwambia mtoto wake: Weka chungu kikubwamotoni, uwapikie hawa wanafunzi wa wafumbuaji chakula. Mmoja akaenda shambani, akachuma mboga, akaona mtango wa mwituni, akachuma kwake hayo matango ya mwituni, akaijaza nguo yake, kisha akaja, akayakatakata chunguni kuwa chakula, kwani hawakuyajua. Kisha wakawaita watu, waje kula. Ikawa, walipokila chakula hicho wakalia kwamba: Kifo kimo chunguni, wewe mtu wa Mungu! Hawakuweza kula. Akasema: Leteni unga! Akautupa chunguni, akasema: Wapakulieni watu hawa, wapate kula! Hakikuwamo tena mle chunguni kilichokuwa kibaya. Kisha akaja mtu kutoka Baali-Salisa, akamletea yule mtu wa Mungu mikate ya malimbuko, nayo ilikuwa mikate ishirini ya mawele, tena gunia lenye masuke mabichi, akasema: Wapeni, watu hawa wale! Mtumishi wake akamwambia: watu mia niwaandalie hii mikate namna gani? Akasema: Wape tu watu hawa, wale! Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Watakula, kisha wasaze. Ndipo, alipowaandalia, wakala, wakasaza, kama Bwana alivyosema. *Namani, mkuu wa vita wa mfalme wa Ushami, alikuwa mtu mkubwa machoni pa bwana wake na mtu mwenye macheo, kwani Bwana alimtumia, awapatie Washami wokovu. Huyu mtu aliyekuwa fundi wa vita mwenye nguvu akaugua ukoma. Siku zilizopita, Washami walipokuwa wametoka kwao vikosi kwa vikosi, waliteka katika nchi ya Waisiraeli mtoto mdogo wa kike, naye akamtumikia mkewe Namani. Huyu akamwambia bibi wake: Kama bwana wangu angemtokea mfumbuaji alioko huko Samaria, yeye angemponya ukoma wake. Ndipo, Namani alipokwenda kwa bwana wake kumsimulia kwamba: Yule mtoto aliyetoka katika nchi ya Waisiraeli amesema hivi na hivi. Mfalme wa Ushami akasema: Haya! Nenda huko! Nami nitakupa barua kwa mfalme wa Waisiraeli. Akaenda akichukua mkononi mwake vipande 10 vya fedha, ndio shilingi 120000 na vipande vidogo vya dhahabu 6000, ndio shilingi 450000 na nguo 10 za sikukuu. Akampelekea mfalme wa Waisiraeli ile barua iliyosema: Hapo, barua hii itakapofika kwako, utamwona mtumishi wangu Namani, ninayemtuma kwako, umponye ukoma wake. Ikawa, mfalme wa Waisiraeli alipoisoma barua hii, akayararua mavazi yake na kusema: Je? Mimi ni Mungu, niweze kuua na kurudisha uzimani, huyu akimtuma mtu wake kwangu, nimponye ukoma wake? Jueni hili, mwone, jinsi huyu anavyonichokoza! Ikawa, Elisa, yule mtu wa Mungu, alipoyasikia, ya kuwa mfalme wa Waisiraeli ameyararua mavazi yake, akatuma kwa mfalme kumwambia: Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje kwangu, apate kujua, ya kuwa katika Waisiraeli yuko mfumbuaji. Ndipo, Namani alipokuja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni penye nyumba ya Elisa. Elisa akatuma mjumbe kwake kumwambia: Nenda koga mara saba mle Yordani! Ndivyo, nyama za mwili wako zitakavyokuwa nzuri tena, nawe utatakata. Ndipo, Namani alipojiendea na kukasirika, akasema: Nimewaza moyoni kwamba: Atanitokea, asimame na kulitambikia Jina la Bwana Mungu wake, kisha pagonjwa apabandikie mkono wake, auponye ukoma. Tena ile mito ya Damasko, Abana na Paripari, siyo mizuri kuliko maji yote ya Isiraeli? Siwezi koga humo, nipate kutakata? Kwa hiyo akageuka, akaenda zake na kuchafuka. Lakini watumishi wake wakamsogelea, wakamwambia: Baba, kama mfumbuaji angalikuambia neno kubwa, hungalilifanya? Tena je? Akikuambia: Nenda koga, upate kutakata, usilifanye? Basi, akashuka, akajizamisha mara saba mle Yordani, kama yule mtu wa Mungu alivyomwambia; ndipo, nyama za mwili wake ziliporudi kuwa kama za mtoto, akatakata. Kisha akarudi kwa yule mtu wa Mungu, yeye nao wote, aliosafiri nao, akaja, akasimama mbele yake, akasema: Nitazame! Ninajua, ya kuwa hakuna Mungu katika nchi zote, isipokuwa katika nchi ya Isiraeli. Sasa pokea matunzo mkononi mwa mtumishi wako! Akajibu: Hivyo, Bwana, ninayemtumikia, alivyo Mwenye uzima, sitachukua cho chote. Akamhimiza, ayachukue, lakini akakataa. Namani akasema: Kama hutaki, basi, lakini mtumishi wako na apewe mzigo wa mchanga unaochukulika na nyumbu wawili, kwani mtumishi wako hatatolea tena miungu mingine ng'ombe au vipaji vingine vya tambiko, ila Bwana peke yake. Neno hili tu Bwana na amwondolee mtumishi wako, bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni kutambika mle, naye akijiegemeza mkononi pangu, akijiangusha chini mle nyumbani mwa Rimoni, nami nikijiangusha chini mle nyumbani mwa Rimoni. Basi, neno hili Bwana na amwondolee mtumishi wako! Akamwambia: Jiendee na kutengemana! Ndipo, alipotoka kwake.* Alipokwisha kwenda kipande kizima, ndipo, Gehazi, mtoto wa Elisa, yule mtu wa Mungu, aliposema: Mbona bwana wangu amemwacha huyu Mshami Namani, asizichukue mkononi mwake zile mali, alizozileta! Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, mimi nitapiga mbio, nimfuate, nichukue mojamoja kwake. Basi, Gehazi akakimbia akimfuata Namani. Namani alipomwona, akimfuata mbiombio, Namani akaruka kutoka garini, akamwendea, akamwuliza: Ni habari njema? Akasema: Ni njema; bwana wangu amenituma kwamba: Tazama, sasa hivi wamekuja kwangu vijana wawili waliotoka milimani kwa Efuraimu kwa wanafunzi wa wafumbuaji. Wape kipande cha fedha, ndio shilingi 12000 na nguo mbili za sikukuu! Namani akamwambia: Itafaa, uchukue vipande viwili vya fedha, ndio shilingi 24000; akamhimiza sana, akazifunga zile fedha katika mifuko miwili pamoja na nguo mbili za sikukuu, akampa nao vijana wawili, wamchukulie. Alipofika kilimani akazichukua mikononi mwao, akaziweka mle nyumbani; nao wale watu akawapa ruhusa, wakaenda zao. Naye alipoingia kumtumikia bwana wake, Elisa akamwuliza: Unatoka wapi, Gehazi? Akajibu: Mtumishi wako hakwenda huko wala huko. Akamwambia: Roho yangu haikwenda na wewe, yule mtu alipogeuka garini mwake, akuone? Je? Siku hii ni siku ya kuchukua fedha na nguo za sikukuu na mashamba ya michekele na ya mizabibu na mbuzi na kondoo na ng'ombe na watumwa na vijakazi? Ukoma wa Namani utakuambukiza wewe na vizazi vyako kale na kale. Alipotoka kwake alikuwa mwenye ukoma uliong'aa kama theluji. Wanafunzi wa wafumbuaji wakamwambia Elisa: Tazama, mahali hapa, tunapokaa machoni pako, ni padogo, hatuenei hapa. Na twende Yordani, tuchukue huko kila mtu nguzo moja, tujitengenezee huko mahali pa kukaa. Akajibu: Nendeni! Mmoja wao akasema: Ingefaa, wewe uende pamoja na watumishi wako. Akasema: Basi, nami nitakwenda. Akaenda nao; walipofika Yordani, wakakata miti. Ikawa, mmoja alipokata nguzo yake, chuma cha shoka yake kikaanguka majini, akalia kwamba: E bwana wangu! Nacho kimekopwa kwa mtu! Yule mtu wa Mungu akauliza: Kimeangukia wapi? Alipomwonyesha pale mahali, akakata kijiti, akakitupa hapohapo; ndivyo, alivyokieleza kile chuma. Kisha akamwambia: Kiokote! Naye akaunyosha mkono wake, akakikamata. Mfalme wa Ushami akawa akiwapelekea Waisiraeli vita. Lakini kila alipopatana na watumishi wake kwamba: Nitapiga makambi yangu mahali fulani, yule mtu wa Mungu akatuma kwa mfalme wa Waisiraeli kumwambia: Angalia, usipitie mahali hapo! kwani ndiko, Washami watakakoshukia. Kwa hiyo mfalme wa Waisiraeli alipotaka kutuma watu kwenda mahali pale, yule mtu wa Mungu alipomkataza, akapona hapo, tena si mara moja wala mbili tu. Ndipo, moyo wa mfalme wa Ushami ulipochafuka kwa ajili hiyo, akawaita watumishi wake, akawauliza: Hamwezi kuniambia, kama ni nani wa kwetu aliye upande wa mfalme wa Waisiraeli? Mmoja wao watumishi wake akasema: Sivyo, bwana wangu mfalme, kwani mfumbuaji Elisa alioko kwao Waisiraeli humsimulia mfalme wa Waisiraeli nayo maneno, unayoyasema chumbani mwako mwa kulalia. Ndipo, alipoagiza: Nendeni kutazama, aliko! Kisha nitatuma kumkamata. Alipopashwa habari kwamba: Yuko Dotani, akatuma kikosi kikubwa chenye farasi na magari kwenda huko; wakafika usiku, wakauzunguka ule mji. Mtumishi wa yule mtu wa Mungu alipoamka asubuhi, aondoke kutoka nje, akaona, ya kuwa kiko kikosi kinachouzunguka huo mji pamoja na farasi na magari; ndipo, yule mtoto wake alipomwambia: E bwana wangu, tufanyeje? Akajibu: Usiogope! Kwani walio upande wetu ndio wengi kuliko wao walio upande wao. Kisha Elisa akaomba na kusema: Bwana, mfumbue macho, apate kuona! Ndipo, Bwana alipomfumbua yule kijana macho, apate kuona, akaona, ya kuwa huo mlima wote umejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisa pande zote. Wale askari walipomshukia, Elisa akamwomba Bwana kwamba: Wapige wamizimu hawa, wapofuke! Akawapiga, wakapofuka, kama Elisa alivyoomba. Kisha Elisa akawaambia: Njia hii siyo, wala mji huu sio; nifuateni, niwapeleke huko, yule mtu, mnayemtafuta, aliko! Akawapeleka Samaria. Walipofika Samaria, Elisa akasema: Bwana, wafumbue watu hawa macho! Ndipo, Bwana alipowafumbua macho, wakaona, ya kuwa wameingia katikati ya mji wa Samaria. Mfalme wa Waisiraeli alipowaona akamwuliza Elisa: Baba, niwapige? Ukisema, nitawapiga! Akajibu: Usiwapige! Je? Uliowateka kwa upanga wako na kwa upindi wako huwapiga? Waandalie vyakula na vya kunywa, wale, wanywe, kisha waende zao kwa bwana wao! Ndipo, alipowatengenezea karamu kubwa, wakala, wakanywa; kisha akawapa ruhusa, wakaenda zao kwa bwana wao. Kisha vikosi vya Ushami havikurudi tena kuingia katika nchi ya Waisiraeli. Hayo yalipokwisha kufanyika, Benihadadi, mfalme wa Ushami, akavikusanya vikosi vyake vyote, akapanda, akausonga Samaria kwa kuuzinga. Mle Samaria ikajamo njaa kubwa; hapo, walipousonga kwa kuuzinga, kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa fedha 80, ndio shilingi 320, nacho kibaba cha mavi ya njiwa kikapata fedha 5, ndio shilingi 20. Siku moja mfalme alipotembea bomani, mwanamke akamlilia kwamba: Bwana wangu mfalme, nisaidie! Akajibu: Bwana asipokusaidia, mimi nitawezaje kukusaidia? Je? Ninacho kitokacho penye kupuria ngano au penye kukamulia zabibu? Kisha mfalme akamwuliza: Shauri lako nini? Akasema: Huyu mwanamke mwenzangu aliniambia: Nipe mwanao, tumle leo! Kisha kesho tutamla wangu. Basi, tukampika mwanangu, tukamla. Tena kesho yake, nilipomwambia: Nipe mwanao, tumle! akamficha. Mfalme alipoyasikia maneno ya huyu mwanamke, akayararua mavazi yake papo hapo, alipokuwa anatembea bomani; nao watu walipomtazama, wakaona, ya kuwa amevaa gunia ndani penye mwili wake. Akasema: Mungu anifanyizie hivi na hivi, Elisa, mwana wa Safati, akishinda leo mwenye kichwa chake! Naye Elisa alikuwa akikaa nyumbani mwake, nao wazee walikaa kwake. Lakini mfalme alikuwa ametuma mtu kwenda mbele yake; huyu mjumbe alipokuwa hajafika bado kwake, yeye Elisa akwaambia wazee: Je? mmeona, ya kuwa amemtuma huyu mwuaji, anikate kichwa? Angalieni! Mjumbe atakapofika, fungeni mlango na kumzuia mlangoni! Je? Hili silo shindo la miguu ya bwana wake anayemfuata? Angali akisema nao, mara mjumbe yule akashuka kufika kwake, akasema: Tazameni, mabaya haya yametoka kwake Bwana! Iko nini tena, tutakayongojea, itoke kwake Bwana? Elisa akasema: Sikilizeni neno la Bwana! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kesho saa zizi hizi pishi ya unga wa ngano itauzwa kwa shilingi mbili na pishi mbili za mawele kwa shilingi mbili hapo mlangoni pa mji huu wa samaria. Ndipo, mkuu wa askari thelathini, ambaye mfalme alimwegemea mkono wake, alipomjibu yule mtu wa Mungu akisema: Ijapo, Bwana aweke madirisha mbinguni, neno hilo litawezekanaje? Akamjibu: Tazama, na uvione mwenyewe kwa macho yako, lakini hutakula wewe. Kulikuwa na watu wanne wenye ukoma waliokaa hapo pa kuliingilia lango la mji, wakasemezana wao kwa wao: Sisi tunakalia nini huku, hata tutakapokufa? Tukisema: Tuingie mjini, njaa imo, nasi tutakufa; tukikaa huku, tutakufa vilevile. Sasa twende, tujipenyeze makambini kwa Washami! Wasipotuua, tutapona; wakituua, basi, tutakufa. Kulipokwisha kuwa usiku, wakaondoka kuingia katika makambi ya Washami, Walipofika pembeni kwa makambi ya Washami. Wakitazama, hamna watu. Kwani Bwana alikuwa amevumisha kwenye makambi ya Washami sauti kama mashindo ya kikosi kikubwa chenye farasi na magari; ndipo, waliposemezana wao kwa wao: Kumbe mfalme wa Waisiraeli ametuletea wafalme wa Wahiti wa wafalme wa Misri, aliowakodisha, watujie! Basi, wakaondoka papo hapo usiku, wakakimbia na kuyaacha mahema yao na farasi wao na punda wao na makambi yote hivyo, yalivyokuwa, wakakimbilia tu kujiponya wenyewe. Ikawa, wale wenye ukoma walipofika pembeni kwa makambi, wakaingia katika hema moja, wakala, wakanywa, wakachukua humo fedha na dhahabu na nguo; kisha wakaenda, wakazichimbia mchangani. Waliporudi wakaingia katika hema jingine, namo humo wakachukua mali, kisha wakaenda kuzichimbia nazo mchangani. Kisha wakasemezana wao kwa wao: Tunayoyafanya siyo! Leo ni siku ya mbiu njema, lakini sisi tukinyamaza tu na kungoja, mpaka kuche, tutakora manza. twenda sasa hivi kupasha habari nyumbani mwa mfalme! Wakaja, wakamwita mngoja lango la mji, wakawapasha habari kwamba: Tumeingia makambini mwa Washami, lakini hamna mtu wala sauti ya mtu, wamo farasi tu waliofungwa na punda waliofungwa, tena mahema yamo vivyo hivyo, yalivyoachwa. Ndivyo, walivyowaitia wangoja lango la mji, nao wakapasha habari mjini nyumbani mwa mfalme. Mfalme alipoamka usiku akawaambia watumishi wake: nitawaelezea haya, Washami waliyotufanyizia: Kwa kuwa wanajua, ya kuwa tuko na njaa, wametoka makambini, wajifiche porini kwamba: Watakapotoka mjini, tutawakamata, wakiwa wa hai, kisha tutaingia mjini. Mmoja wao watumishi wake akamjibu akisema: Chukueni farasi watano waliosalia katika wao waliosazwa humu mjini, kwani nao ni sawa kama wale Waisiraeli wengi mno waliosazwa humu mjini, maana nao watakuwa wa kufa tu kama wale Waisiraeli wengi waliokwisha kumalizika. Kwa hiyo na tuwatume, tuone yatakayokuwa. Wakachukua magari mawili yenye farasi, ndiyo, mfalme aliyoyatuma kuwafuata Washami waliotoka makambini, akawaambia: Nendeni, mwatazame! Wakawafuata mpaka kwenye Yordani, wakaona, njia hiyo yote imejaa mavazi na mata, Washami waliyoyaacha wakikimbia upesiupesi. Ndipo, wale wajumbe waliporudi kumpasha mfalme habari. Basi, watu wakatoka mjini, wakayateka makambi ya washami. Kisha pishi ya unga wa ngano ikauzwa kwa shilingi mbili na pishi mbili za mawele kwa shilingi mbili, kama Bwana alivyosema. Yule mkuu wa askari thelathini, ambaye mfalme alimwegemea mkono wake, akamweka langoni mwa mji, awasimamie watu, lakini watu wakamkanyaga mle langoni, akafa palepale, kama yule mtu wa Mungu alivyosema hapo, mfalme aliposhuka kufika kwake. Hapo yakawa yaleyale, yule mtu wa Mungu aliyomwambia mfalme kwamba: Kesho saa zizi hizi pishi ya unga wa ngano itauzwa kwa shilingi mbili na pishi mbili za mawele kwa shilingi mbili hapa langoni pa mji huu wa Samaria. Ndipo, yule mkuu wa askari thelathini alipomjibu yule mtu wa Mungu akisema: Ijapo, Bwana aweke madirisha mbinguni, neno hilo litawezekanaje? Naye yule alikuwa amemjibu: Tazama, na uvione mwenyewe kwa macho yako, lakini hutakula wewe. Ndiyo yaliyotimia hapo, watu walipomkanyaga penye lango la mji, mpaka akifa. Elisa alikuwa amesema na yule mwanamke, aliyemfufulia mwanawe, akamwambia: Ondoka, uende wewe na mlango wako, ukae ugenini kutakakokufalia kukaa ugenini! Kwani Bwana ameita njaa, ije kuiingia hata nchi hii miaka saba. Ndipo, yule mwanamke alipoondoka, akafanya, kama yule mtu wa Mungu alivyomwambia, akaenda yeye na mlango wake, akakaa ugenini katika nchi ya Wafilisti miaka saba. Hiyo miaka saba ilipokwisha pita, yule mwanamke akaondoka tena katika nchi ya Wafilisti, akarudi, akamtokea mfalme kumlilia kwa ajili ya nyumba yake na ya shamba lake. Hapo mfalme alikuwa akisema na Gehazi aliyekuwa naye yule mtu wa Mungu kwamba: Nisimulie matendo makubwa yote, Elisa aliyoyafanya! Naye akawa akimsimulia mfalme, jinsi alivyomrudisha yule mfu uzimani, mara yule mwanamke, aliyemfufulia mwanawe, akawako akimlilia mfalme kwa ajili ya nyumba yake na ya shamba lake. Ndipo, Gehazi alipomwambia: Bwana wangu mfalme, huyu ndiye yule mwanamke, naye huyu ndiye mwanawe, Elisa aliyemfufua. Mfalme alipomwuliza huyu mwanamke, naye akamsimulia yote. Ndipo, mfalme alipompa mtumishi mmoja wa nyumbani, akamwagiza: Mrudishie yote yaliyokuwa yake nayo mapato yote ya shamba yaliyopatikana tangu sike ile, alipoiacha nchi hii, hata sasa. Kisha Elisa akaja Damasko, naye Benihadadi, mfalme wa Ushami, alikuwa mgonjwa, akapashwa habari, ya kuwa yule mtu wa Mungu amefika huko. Ndipo, mfalme alipomwambia Hazaeli: Chukua matunzo mkononi mwako, uende kuonana na yule mtu wa Mungu, umwombe, aniulizie kwa Bwana, kama nitapona ugonjwa huu. Hazaeli akaenda kuonana naye akichukua mkononi mwake matunzo yote yaliyokuwa vitu vizuri vya Damasko, ya kuchukuliwa na ngamia 40. Alipofika akaja kusimama mbele yake, akamwambia: Mwanao Benihadadi, mfalme wa Ushami, amenituma kwako kukuuliza kwamba: Nitapona ugonjwa huu? Elisa akamjibu: Nenda kumwambia: Kupona utapona; lakini Bwana amenionyesha, ya kuwa atakufa. Kisha yule mtu wa Mungu akamng'arizia macho na kulia machozi, hata mwenyewe akiona soni kwa kufanya hivyo. Hazaeli akamwuliza: Mbona bwana wangu analia machozi? Akajibu: Kwani ninajua, ya kama utawafanyizia wana wa Isiraeli mabaya, miji yao yenye maboma utaiteketeza kwa moto, vijana wao wenye nguvu utawaua kwa panga, wachanga wao utawaponda nao wanawake wao wenye mimba utawatumbua. Hazaeli akasema: Mtumwa wako, huyu mbwa, ni mtu gani, aweze kufanya mambo makuu kama hayo? Elisa akasema: Bwana amenionyesha, ya kuwa wewe utakuwa mfalme wa Ushami. Kisha akatoka kwake Elisa, akaja kwa bwana wake, naye akamwuliza: Elisa amekuambia nini? Akajibu: Ameniambia, ya kuwa utapona. Kesho yake akachukua tandiko la kitanda, akalichovya majini, kisha akamfunika uso nalo, hata akafa. Naye Hazaeli akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 5 wa Yoramu, mwana wa Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, Yosafati alipomaliza kuwa mfalme wa Wayuda, Yoramu, mwana wa Yosafati, akapata kuwa mfalme wa Wayuda. Alikuwa mwenye miaka 32 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 8. Naye akaendelea katika njia za wafalme wa Waisiraeli, kama wale wa mlango wa Ahabu walivyofanya, kwani binti Ahabu alikuwa mkewe, akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana. Lakini Bwana hakutaka kuwaangamiza Wayuda kwa ajili ya mtumishi wake Dawidi, kwa kuwa alimwambia, ya kama atampa yeye na wanawe kuwa taa iwakayo siku zote. Katika hizo siku zake Waedomu wakalivunja agano wakijitoa mikononi mwa Wayuda, wakajiwekea mfalme wa kuwatawala. Ndipo, Yoramu alipoondoka kwenda Sairi akiyachukua magari yote; ikawa, alipoondoka usiku, akawapiga Waedomu waliomzunguka yeye na wakuu wa magari lakini watu walikuwa wameyakimbilia mahema yao. Lakini Waedomu wakalivunja agano tena, wakajitoa mikononi mwa Wayuda mpaka siku hii ya leo. Kisha nao wa Libuna wakalivunja agano siku zilezile. Mambo mengine ya Yoramu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Yoramu akaja kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Ahazia akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 12 wa Yoramu, mwana wa Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, Ahazia, mwana wa Yoramu, akapata kuwa mfalme wa Wayuda. Ahazia alikuwa mwenye miaka 22 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu mwaka mmoja. Jina la mama yake ni Atalia, binti Omuri, mfalme wa Waisiraeli. Naye akaendelea katika njia ya mlango wa Ahabu, akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kama mlango wa Ahabu. Kwani yeye alikuwa mkwe wao wa mlango wa Ahabu. Akaenda pamoja na Yoramu, mwana wa Ahabu, kumpelekea Hazaeli, mfalme wa Ushami, vita huko Ramoti wa Gileadi, lakini Washami wakamwumiza Yoramu. Kwa hiyo mfalme Yoramu akarudi Izireeli, apate watakaomponya vidonda, Washami walivyompiga kule Rama, alipopigana na Hazaeli, mfalme wa Ushami. Ndipo, Ahazia, mwana wa Yoramu, mfalme wa Wayuda, aliposhuka kumtazama Yoramu, mwana wa Ahabu, huko Izireeli, kwani ndiko, alikougulia. Mfumbuaji Elisa akamwita mmoja wao wanafunzi wa wafumbuaji, akamwambia: Jifunge viuno vyako, kisha kichukue kichupa hiki cha mafuta mkononi mwako, uende Ramoti wa Gileadi! Utakapofika huko, umtazame huko Yehu, mwana wa Yosafati, mwana wa Nimusi, kisha ingia mwake, umwondoe kwenye ndugu zake na kumwingiza katika chumba cha ndani! Kisha kichukue hicho kichupa cha mafuta, uyamimine kichwani pake na kumwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nimekupaka mafuta, uwe mfalme wa Waisiraeli. Kisha fungua mlango, ukimbie pasipo kukawia! Ndipo, yule kijana aliyekuwa mfumbuaji kijana alipokwenda Ramoti wa Gileadi. Alipofika akawakuta wakuu wa vikosi, wakikaa pamoja, akasema: Niko na neno la kukuambia wewe mkuu. Yehu alipomwuliza: Mkuu gani kwetu sisi sote? akajibu: Wewe mkuu. Ndipo, alipoondoka, akaingia nyumbani; humo akayamimina yale mafuta kichwani pake na kumwambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Nimekupaka mafuta, uwe mfalme wao Waisiraeli walio ukoo wake Bwana. Utawaua walio wa mlango wa bwana wako Ahabu, nipate kuzilipiza damu za wafumbuaji waliokuwa watumishi wangu, nazo damu za watumishi wote wa Bwana nikizitaka mkononi mwa Izebeli. Mlango wote wa Ahabu utaangamia, nitakapowatowesha kwao wa Ahabu wote walio wa kiume, kama watakuwa wamefungwa au kama watakuwa wamefunguliwa kwao Waisiraeli. Nitautoa mlango wa Ahabu, uwe kama mlango wa Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kama mlango wa Basa, mwana wa Ahia. Naye Izebeli mbwa watamla shambani kwa Izireeli, pasiwepo atakayemzika. Kisha akafungua mlango, akakimbia. Yehu alipotokea kwao watumishi wa bwana wake, wakamwuliza: Ni habari njema? Mbona huyo mwenye wazimu ameingia mwako? Akawajibu: Mnamjua yule mtu na maneno yake. Wakamwambia: Uwongo huu! Tupashe habari zake! Ndipo, aliposema: Amesema hivi na hivi, akaniambia kwamba: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana: Nimekupaka mafuta, uwe mfalme wa Waisiraeli. Ndipo, wote walipozivua nguo zao upesi, wakaziweka miguuni pake juu ya vipago, zivifunike, wakapiga baragumu kwamba: Yehu ni mfalme! Kisha Yehu, mwana wa Yosafati, mwana wa Nimusi, akamlia Yoramu njama. Ni hapo, Yoramu alipokuwa akiulinda mji wa Ramoti wa Gileadi, yeye na Waisiraeli wote, usichukuliwe na Hazaeli, mfalme wa Ushami. Lakini mfalme Yoramu alikuwa amerudi Izireeli, apate watakaomponya vidonda, Washami walivyompiga, alipopigana na Hazaeli, mfalme wa Ushami. Basi, Yehu akawaambia: Kama ndivyo, roho zenu nazo zinavyotaka, asiponyoke mtu wa kutoka humu mjini kwenda Izireeli na kuzipeleka habari hizi. Kisha Yehu akalipanda gari lake kwenda Izireeli, kwani ndiko, Yoramu alikougulia, naye Ahazia, mfalme wa Wayuda, alikuwa ameshuka kumtazama Yoramu. Mlinzi aliyesimama mnarani juu kule Izireeli alipoliona kundi zima la Yehu, likija, akasema: Mimi naona kundi zima la watu! Ndipo, Yoramu alipomwambia: Chukua mpanda farasi, mtume kuwaendea njiani, awaulize: Mwaleta habari njema? Kwa hiyo mpanda farasi akamwendea njiani, akamwambia: Hivi ndivyo, mfalme anavyouliza: Waleta habari njema? Yehu akajibu: Unatuulizaje habari? Zunguka, unifuate! Ndipo, mlinzi alipoleta habari kwamba: Yule mjumbe amefika kwao, lakini hakurudi. Basi, akatuma mpanda farasi wa pili; naye alipofika kwao akasema: Hivi ndivyo, mfalme anavyouliza: Waleta habari njema? Yehu akajibu: Unatuulizaje habari? Zunguka, unifuate! Mlinzi akapasha habari tena kwamba: Amefika kwao, lakini hakurudi. Lakini ile namna ya kuendesha gari ni kama ya Yehu, mwana wa Nimusi, kwani analiendesha gari lake kama mwenye wazimu. Ndipo, Yoramu alipoagiza, wafunge farasi penye magari; walipokwisha kulifungia gari lake farasi, Yoramu, mfalme wa Waisiraeli, akatoka pamoja na Ahazia, mfalme wa Wayuda, kila mmoja katika gari lake, kumwendea Yehu njiani; wakamkuta penye shamba la Naboti wa Izireeli. Yoramu alipomwona Yehu akamwuliza: Waleta habari njema, Yehu? Akajibu: Ni habari gani njema? Ugoni wa mama yako Izebeli na uchawi wake si mwingi? Ndipo, Yoramu alipoligeuza gari kwa mikono yake, akakimbia na kumwambia Ahazia: Tumedanganyika, Ahazia. Yehu akaushika upindi kwa mkono wake, akauvuta kwa nguvu, akampiga Yoramu katikati ya mabega yake, mshale ukatokea moyoni mwake, akaangukia magotini garini mwake. Kisha akamwagiza Bidekari aliyekuwa mkuu wa askari thelathini: Mchukue, umtupe penye shamba la Naboti wa Izireeli! Kumbuka, mimi na wewe tulipomfuata baba yake Ahabu na kupanda farasi sisi wawili, hapo Bwana alilitoa tamko lile la kumtisha kwamba: Ndivyo, asemavyo Bwana: Damu ya Naboti nazo damu za wanawe, nilizoziona jana, nitakulipisha huku kwenye shamba hili; ndivyo, asemavyo Bwana. Sasa mchukue, umtupe katika shamba hilo, kama Bwana alivyosema. Ahazia, mfalme wa Wayuda, alipoviona akakimbia na kuishika njia ya Beti-Hagani (Nyumba ya Bustani), Yehu akamfuata mbiombio, akaagiza: Naye mpigeni katika gari lake! Wakampiga hapo pa kupandia Guri karibu ya Ibileamu; akakimbia hata Megido, ndiko alikokufa. Watumishi wake wakampeleka Yerusalemu katika gari lake, wakamzika katika kaburi lake kwa baba zake mjini mwa Dawidi. Huyu Ahazia alikuwa ameupata ufalme wa Wayuda katika mwaka wa 11 wa Yoramu, mwana wa Ahabu. Kisha Yehu akaja Izireeli. Izebeli alipoyasikia, akatia wanja machoni pake, akakipamba nacho kichwa chake vizuri, kisha akachungulia dirishani. Yehu alipoingia langoni mwa mji, akamwuliza: Zimuri aliyemwua bwana wake hajambo? Ndipo, alipouelekeza uso wake kwenye lile dirisha na kuuliza: Yuko nani aliye upande wangu? Alipowaona watumishi wa nyumbani wawili au watatu, wakimchungulia, akaagiza: Msukumeni! Wakamsukuma na kumbwaga chini, ukuta ukaenea damu yake, nao farasi vilevile, nao wakamkanyaga. Yehu alipokwisha kuingia, akala, akanywa, kisha akaagiza: Haya! Mtazameni yule mwanamke aliyeapizwa, mmzike, kwani ni binti mfalme. Walipokwenda kumzika hawakumwona, ni kichwa tu na miguu na viganja vya mikono. Wakarudi kumpasha hizi habari; ndipo, aliposema: Hivi ndivyo, Bwana alivyosema kinywani mwa Elia wa Tisibe kwamba: Shambani kwa Izireeli mbwa watazila nyama za mwili wake Izebeli. Nao mzoga wake Izebeli utakuwa kama kinyesi cha shambani katika viwanja vya Izireeli, watu wasiweze kusema: Huyu hapa ni Izebeli. Ahabu alikuwa na wana 70 kule Samaria. Kwa ajili yao Yehu akaandika barua, akazituma Samaria kwa wakuu wa Izireeli na kwa wazee na kwa watunzaji wa wana wa Ahabu kwamba: Kwa kuwa mnao wana wa bwana wenu na magari na farasi na maboma na mata, basi, barua hii itakapofika, kwenu, mtazameni aliye mwema mwenye unyofu katika wana wa bwana wenu, mkalisheni katika kiti cha kifalme cha baba yake, kisha mwupigie vita mlango wa bwana wenu! Wakashikwa na woga sanasana, wakasema: Wale wafalme wawili hawakuweza kusimama usoni pake, nasi tutawezaje kusimama? Kwa hiyo wale waliousimamia ule mlango na mji pamoja na wazee na watunzaji wa wana wakatuma kwa Yehu kumwambia: Sisi tu watumwa wako, nayo yote, utakayotuagiza, tutayafanya, lakini hatuwezi kumweka mtu kuwa mfalme; fanya tu yaliyo mema machoni pako! Akawaandikia barua ya pili kwamba: Kama ninyi ni watu wangu, kama ninyi mnataka kunisikia, nikiwaambia neno, vitwaeni vichwa vya wana wa bwana wenu, mvilete kwangu Izireeli kesho saa hizi! Nao wana wa mfalme, wakuu wa mji waliowakuza, walikuwa 70. Barua hii ilipofika kwao, wakawachukua wana wa mfalme, wakawachinja wote 70, navyo vichwa vyao wakavitia katika makapu, wakavituma kwake Izireeli. Mjumbe alipokwenda kumpasha habari, ya kuwa wamevileta vichwa vya wana wa mfalme, akasema: Viwekeni machungu mawili hapo pa kuingia langoni mwa mji mpaka kesho! Ikawa, alipotoka asubuhi akasimama hapo, akawaambia watu wote: Ninyi hamna kosa lo lote. Nitazameni mimi! Mimi nimemlia bwana wangu njama, nikamwua. Lakini aliyewaua hawa wote ni nani? Hapa jueni, ya kuwa hakuna neno lo lote la Bwana, Bwana alilolisema la mlango wa Ahabu, lililoanguka chini, kwani Bwana anayafanya, aliyoyasema kinywani mwa mtumishi wake Elia. Ndipo, Yehu alipowaua wote waliosalia wa mlango wa Ahabu huko Izireeli nao wakuu wake wote na rafiki zake wote na watambikaji wake wote, kwao hakusazwa hata mmoja aliyepona. Kisha akaondoka, akaenda Samaria. Alipofika njiani penye nyumba, wachungaji walimokatia manyoya ya kondoo, Yehu akawakuta ndugu zake Ahazia, mfalme wa Wayuda, akawauliza: Ninyi wa nani? Wakajibu: Sisi ndugu zake Ahazia, tukashuka kuamkiana nao wana wa mfalme na wana wa bibi wake mfalme. Ndipo, alipoagiza: Wakamateni hivyo, walivyo hai! Wakawakamata hivyo, walivyokuwa hai, wakawachinja hapo penye kisima cha hiyo nyumba, walimokatia manyoya ya kondoo, watu 42, hakusaza hata mmoja wao. Alipoondoka huko, akamkuta Yonadabu, mwana wa Rekabu, aliyekuja kuonana naye, akamwuliza: Moyo wako unanielekea, kama moyo wangu unavyouelekea moyo wako? Yonadabu alipojibu: Ndio, akasema: Kama ndivyo, nipe mkono wako! Alipompa mkono wake akampandisha garini mwake, akamwambia: Twende pamoja, uone wivu wangu, nilio nao kwa ajili ya Bwana! Kisha akaenda naye garini mwake. Alipofika Samaria, akawaua wote waliosalia huko Samaria wa mlango wa Ahabu, mpaka akiwaangamiza kabisa kwa lile neno la Bwana, alilomwambia Elia. Yehu akawakusanya watu wote, akawaambia: Ahabu alimtumikia Baali kidogo tu, lakini Yehu atamtumikia kabisa. Sasa waiteni wafumbuaji wote wa Baali na watumishi wake wote na watambikaji wake wote, waje kwangu, asikoseke hata mmoja! Kwani ninataka kumtolea Baali ng'ombe nyingi za tambiko; kila atakayekoseka hatapona. Lakini Yehu aliyafanya haya kwa ujanja, kusudi apate kuwaangamiza wamtumikiao Baali. Kisha Yehu akawaambia: Takaseni mkutano wa kumtambikia Baali! Walipoutangaza, Yehu akatuma kwa Waisiraeli wote, wakaja wote waliomtumikia Baali, hakusalia hata mmoja asiyekuja. Kisha wakaingia nyumbani mwa Baali, nayo hiyo nyumba ya Baali ikajaa watu huku na huko. Kisha akamwagiza msimamizi wa nguo za watu wa mfalme: Wape wote wanaomtumikia Baali kila mmoja vazi moja. Huyu alipokwisha kuwapa hayo mavazi, Yehu akaingia nyumbani mwa Baali pamoja na Yonadabu, mwana wa Rekabu, akawaambia wanaomtumikia Baali: Chunguzeni na kutazama, kusiweko huku kwenu na watumishi wa Bwana, ila wawe wao peke yao wanaomtumikia Baali! Kisha wakaja kutoa vipaji vya tambiko na ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima. Lakini Yehu alikuwa amejiwekea nje watu 80, akawaambia: Mtu atakayepona kwao hao, nitakaowaleta na kuwatia mikononi mwenu, basi, roho yake itakuwa mahali pa roho yake yule. Walipokwisha kuzitoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, Yehu akawaambia wale wapiga mbio na wakuu wa askari thelathini: Ingieni, mwaue, mtu hata mmoja asipate kutoka! Ndipo, wale wapiga mbio na wakuu wa askari thelathini walipowaua kwa ukali wa panga, wakawatupa nje; kisha wakaingia mle ndani nyumbani mwa Baali, wakazitoa nguzo za kutambikia mle nyumbani mwa Baali, wakaziteketeza. Kisha wakaivunjavunja ile nguzo ya mawe ya kumtambikia Baali, nayo nyumba ya Baali wakaivunjavunja, wakaitumia kuwa mahali pa vyoo hata siku hii ya leo. Ndivyo, Yehu alivyoyakomesha matambiko ya Baali kwao Waisiraeli. Lakini makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli, Yehu hakuacha kuyafuata akizitambikia ndama za dhahabu zilizowekwa Beteli na Dani. Bwana akamwambia Yehu: Kwa kuwa umetenda vema ukiyafanya yanyokayo machoni pangu, tena ukiufanyizia mlango wa Ahabu yote yaliyokuwamo moyoni mwangu, kwa hiyo wanao wa vizazi vinne watakaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli. Lakini Yehu hakuangalia kuendelea na kuyashika Maonyo ya Bwana Mungu wa Isiraeli kwa moyo wake wote, wala hakuyaacha makosa ya Yeroboamu aliyewakosesha Waisiraeli. Siku hizo Bwana akaanza kuikatakata nchi ya Waisiraeli, Hazaeli akawapiga Waisiraeli po pote penye mipaka, akaichukua nchi yote ya Gileadi iliyoko ng'ambo ya Yordani upande wa maawioni kwa jua, ndiyo nchi ya Gadi na ya Rubeni na ya Manase kutoka Aroeri ulioko kwenye mto wa Arnoni, hata Gileadi na Basani. Mambo mengine ya Yehu nayo yote, aliyoyafanya, na matendo yake yote ya vitani yaliyokuwa yenye nguvu hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Yehu alipokuja kulala na baba zake, wakamzika Samaria, naye mwanawe Yoahazi akawa mfalme mahali pake. Nazo siku, Yehu alizokuwa mfalme wa Waisiraeli kule Samaria, ni miaka 28. Atalia, mamake Ahazia, alipoona, ya kuwa mwanawe amekufa, akaondoka, akawaangamiza wazao wote wa kifalme. Lakini Yoseba, binti mfalme Yoramu, umbu lake Ahazia, akamchukua Yoasi, mwana wa Ahazia, akamwiba katikati ya wana wa mfalme waliokwenda kuuawa, akamweka pamoja na mnyonyeshaji wake katika chumba cha kulalia. Ndivyo, alivyomficha, Atalia asimwone; kwa hiyo hakuuawa. Akakaa naye na kufichwa Nyumbani mwa Bwana miaka sita, Atalia alipokuwa mfalme wa kike wa nchi hiyo. Katika mwaka wa saba Yoyada akatuma kuwachukua wakuu wa mamia ya askari na wapiga mbio, akawapeleka kwake Nyumbani mwa Bwana, akafanya maagano nao akiwaapisha mle Nyumbani. Kisha akawaonyesha mwana wa mfalme, akawaagiza kwamba: Hili ndilo neno, mtakalolifanya: fungu lenu la tatu watakaoingia kazi siku ya mapumziko na walinde ulinzi wa nyumba ya mfalme; fungu jingine la tatu na walinde penye lango la Suri, nalo fungu jingine la tatu na walinde langoni nyuma ya wapiga mbio! Ndivyo, mtakavyolinda ulinzi wa hiyo nyumba na kuzuia watu. Navyo vikosi vyenu viwili watakaotoka kazini siku ya mapumziko, wote sharti walinde ulinzi wa Nyumba ya Bwana kwake mfalme! Sharti mmzunguke mfalme pande zote kila mtu akiyashika mata yake, kila atakayeingia katika hii mipango ya watu na auawe! Hivyo sharti mwe na mfalme, akitoka, hata akiingia. Wakuu wa mamia wakayafanya yote, kama mtambikaji Yoyada alivyowaagiza; kila mtu akawachukua watu wake walioingia kazi siku ya mapumziko nao waliotoka kazi siku ya mapumziko, wakaja kwa mtambikaji Yoyada. Kisha huyu mtambikaji akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao za mfalme Dawidi zilizokuwamo Nyumbani mwa Bwana. Wakawapanga wapiga mbio, kila mtu na mkuki wake mkononi mwake kuanzia upande wa kuume wa Nyumba kuufikia upande wa kushoto wa Nyumba, kuifikia meza ya kutambikia na tena kuifikia Nyumba yenyewe, wamzunguke mfalme pande zote. Kisha akamtoa mwana wa mfalme, akamvika kilemba cha kifalme, wakampa nacho kizingo cha Ushahidi, wakamfanya kuwa mfalme wakimpaka mafuta. Kisha wakapiga makofi na kusema: Pongezi, mfalme! Atalia alipozisikia sauti za wapiga mbio na za watu, akaja naye hapo, watu walipokuwa, penye Nyumba ya Bwana. Alipotazama, akamwona mfalme, akisimama katika ulingo kama desturi, nao wakuu na wapiga matarumbeta wakisimama kwake mfalme, nao watu wote wa nchi yao wakawa wenye furaha na kupiga matarumbeta. Ndipo, Atalia alipoyararua mavazi yake na kupiga kelele kwamba: Mmedanganyika! Mmedanganyika! Ndipo, mtambikaji Yoyada alipowaagiza wakuu wa mamia waliovisimamia vikosi, akawaambia: Mtoeni hapa penye mipango ya watu! Naye atakayemfuata na auawe kwa upanga! Kwani mtambikaji alisema, asiuawe Nyumbani mwa Bwana. Wakamkamata kwa mikono, naye alipofika penye njia, farasi waliyoishika ya kuingia nyumbani mwa mfalme, akauawa hapo. Kisha Yoyada akafanya agano na Bwana, yeye na mfalme wa watu, wawe ukoo wake Bwana; agano jingine akamfanyia mfalme na watu. Ndipo, watu wote wa nchi hiyo walipoiingia nyumba ya Baali, wakaibomoa, nazo meza za kumtambikia na vinyago vyake wakavivunjavunja kabisa, naye Matani, mtambikaji wa Baali, wakamwua mbele ya meza za kutambikia. Kisha yule mtambikaji akaweka wakaguzi wa Nyumba ya Bwana. Kisha akawachukua wakuu wa mamia nao askari nao wapiga mbio pamoja na watu wote wa nchi hii, wakamtoa mfalme Nyumbani mwa Bwana, wakaingia nyumbani mwa mfalme na kushika njia ya lango la wapiga mbio; ndivyo, alivyopata kukaa katika kiti cha kifalme cha wafalme. Nao watu wote wa nchi hii wakafurahi, nao mji ukatulia. Lakini Atalia walikuwa wamemwua kwa upanga nyumbani mwa mfalme. Naye Yoasi alikuwa mwenye miaka saba alipoupata ufalme. Katika mwaka wa 7 wa Yehu Yoasi akawa mfalme, akaushika ufalme mle Yerusalemu miaka 40, nalo jina la mama yake ni Sibia wa Beri-Seba. Yoasi akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana siku zake zote, mtambikaji Yoyada alizomfundisha. Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, maana watu wakaendelea bado kutoa ng'ombe za tambiko na kuvukiza vilimani pa kutambikia. Yoasi akawaambia watambikaji: Fedha zote zinazoletwa Nyumbani mwa Bwana, ziwe mali za Bwana, kama ni fedha, mtu anazozitoa mwenyewe, au kama ni fedha za kujikomboa, fedha zo zote, mtu atakazowaza moyoni mwake kuzipeleka Nyumbani mwa Bwana, watambikaji na wajitwalie kila mtu kwao, anaojuana nao. Kisha wao wenyewe wapatengeneze, Nyumba ilipobomoka, po pote panapoonekana palipobomoka. Lakini katika mwaka wa 23 wa mfalme Yoasi watambikaji walikuwa hawajapatengeneza bado, Nyumba ilipobomoka. Ndipo, mfalme Yoasi alipomwita mtambikaji Yoyada na watambikaji wengine, akawaambia: Mbona hamjapatengeneza, Nyumba ilipobomoka? Sasa msijitwalie fedha kwao, mnaojuana nao, ila sharti mzitoe za kupatengeneza, Nyumba ilipobomoka. Watambikaji wakaitikia, wasijitwalie tena fedha kwa watu, wala wasipatengeneze wao, Nyumba ilipobomoka. Ndipo, mtambikaji Yoyada alipochukua kasha moja, akatoboa tundu katika kifuniko chake, akaliweka penye meza ya kutambikia kuumeni kwake pa kuingia Nyumbani mwa Bwana; ndimo, watambikaji waliolinda vizingiti walimotia fedha zote zilizoletwa Nyumbani mwa Bwana. Walipoona, ya kuwa fedha zimo nyingi mle kashani, mwandishi wa mfalme na mtambikaji mkuu wakapanda, wakazifunga na kuzihesabu fedha zote zilizooneka Nyumbani mwa Bwana. Fedha zilipokwisha kupimwa zikatiwa mikononi mwao wenye kazi hiyo waliowekwa kuisimamia Nyumba ya Bwana; nao wakazitumia kuwalipa maseremala na mafundi wengine walioijenga Nyumba ya Bwana, kama waashi na wachonga mawe. Tena walizitumia za kununua miti na mawe ya kuchonga ya kupatengeneza, Nyumba ya Bwana ilipobomoka, na kuvilipa vyote vingine vilivyotakiwa vya kuitengeneza Nyumba ya Bwana. Lakini mabakuli ya fedha na makato ya kusafishia mishumaa na vyano na matarumbeta na vyombo vyo vyote vya dhahabu na vya fedha vya kutumiwa Nyumbani mwa Bwana havikutengenezwa kwa zile fedha zilizoletwa Nyumbani mwa Bwana. Kwani waliozipata ni wale tu waliofanya kazi za kuitengeneza Nyumba ya Bwana, Nao hao, waliowapa hizo fedha mikononi mwao, wawalipe wafanya kazi, hawakuzihesabu nao, kwani walifanya kazi zao kwa welekevu. Fedha za tambiko la weuo nazo fedha za tambiko la upozi hazikupelekwa Nyumbani mwa Bwana, zilikuwa mali za watambikaji. Siku zile Hazaeli, mfalme wa Ushami, akapanda, akapiga vita huko Gati; alipokwisha kuuteka, Hazaeli akaulekeza uso wake kuupandia Yerusalemu. Ndipo, Yoasi, mfalme wa Wayuda, alipovichukua vipaji vitakatifu vyote, Yosafati na Yoramu na Ahazia walivyovitoa, viwe mali za Bwana, na vipaji vitakatifu, alivyovitoa yeye, nazo dhahabu zote zilizopatikana katika vilimbiko vya Nyumba ya Bwana namo katika vilimbiko vya nyumba ya mfalme, akampelekea Hazaeli, mfalme wa Ushami; ndipo, alipoondoka Yerusalemu. Mambo mengine ya Yoasi, nayo yote aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Watumishi wake wakamwinukia na kumlia njama, kisha wakamwua Yoasi katika boma la Milo panapotelemkia silo. Watumishi wake, Yozakari, mwana wa simati, na Yozabadi, mwana wa someri, ndio waliomwua; alipokufa, wakamzika kwa baba zake mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Amasia akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 23 wa Yoasi, mwana wa Ahazia, mfalme wa Wayuda, Yoahazi, mwana wa Yehu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli kule Samaria miaka 17. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, akayafuata makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli. Asipoyaepuka, makali ya Bwana yakawawakia Waisiraeli, akawatia mkononi mwa Hazaeli, mfalme wa Ushami, namo mkononi mwa Benihadadi, mwana wa Hazaeli, siku zote. Lakini Yoahazi alipokuwa anamlalamikia Bwana, Bwana akamsikia, kwani aliyaona masongano ya Waisiraeli, kwa kuwa mfalme wa Ushami aliwasonga. Ndipo, Bwana alipowapa Waisiraeli mwokozi, wakatoka mikononi mwa Washami, wana wa Isiraeli wakapata kukaa tena mahemani kwao kama huko kale, Lakini hawakuyaepuka makosa ya mlango wa Yeroboamu aliyewakosesha Waisiraeli, ila wakaendelea kuyafanya, nacho kinyago cha Ashera kilisimama bado mle Samaria. Kwa hiyo Bwana hakusaza kwa Yoahazi watu wa kupiga vita, ni wapanda farasi 50 na magari 10 na watu 10000 waliokwenda kwa miguu, kwani mfalme wa Ushami aliwaangamiza na kuwafananisha na uvumbi ulioko kwenye kupuria. Mambo mengine ya Yoahazi nayo yote, aliyoyafanya, na matendo yake ya vitani yaliyokuwa yenye nguvu hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Yoahazi alipokwenda kulala na baba zake, wakamzika Samaria, naye mwanawe Yoasi akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 37 wa Yoasi, mfalme wa Wayuda, Yoasi, mwana wa Yoahazi, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli kule Samaria miaka 16. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, hakuyaepuka makosa yote ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli, ila akaendelea kuyafanya. Mambo mengine ya Yoasi nayo yote, aliyoyafanya, na matendo yake yenye nguvu, aliyoyatenda alipopiga vita na Amasia, mfalme wa Wayuda, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Yoasi alipokwenda kulala na baba zake, mwanawe Yeroboamu akakaa katika kiti chake cha kifalme, naye Yoasi akazikwa Samaria kwao wafalme wa Waisiraeli. Elisa alipopata ugonjwa wake uliomwua, ndipo, Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, aliposhuka kuja kwake, akalia machozi mbele yake na kusema: Baba yangu! Baba yangu! Wewe gari la Waisiraeli na wapanda farasi wake! Elisa akamwambia: Chukua upindi na mishale! Basi, akajichukulia upindi na mishale. Kisha akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Shika upindi mkononi mwako! Alipoushika mkononi mwake, Elisa akaiweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Kisha akamwambia: Fungua dirisha upande wa maawioni kwa jua! Alipoifungua, Elisa akamwambia: Piga mshale! Alipopiga mshale, akasema: Huu ni mshale wa wokovu wa Bwana, ndio mshale wa kuokoa mikononi mwa Washami. Utawapiga Washami kule Afeki, hata uwamalize. Kisha akasema: Chukua mishale! Alipoichukua, akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Ipige nchi! Akaipiga mara tatu, kisha akasimama. Ndipo, yule mtu wa Mungu alipomkasirikia, akamwambia: Ungaliipiga mara tano au mara sita, ungaliwapiga Washami, hata uwamalize kabisa. Lakini sasa utawapiga Washami mara tatu tu. Elisa alipokwisha kufa, wakamzika. Hapo vikosi vya Wamoabu wakaingia katika nchi hii, nao wakaja kila mwaka. Ikawa, walipotoka, waende kuzika mtu, mara wakaona kikosi; kwa hiyo wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisa. Lakini yule mtu alipofika ndani na kuigusa mifupa ya Elisa, mara akawa mzima tena, akaweza kusimama miguuni pake. Hazaeli, mfalme wa Washami, alikuwa akiwasonga Waisiraeli siku zote za Yoahazi. Kisha Bwana akawawia mpole tena na kuwahurumia, akawaelekea kwa ajili ya Agano lake, alilomwekea Aburahamu na Isaka na Yakobo; kwa hiyo hakutaka kuwaangamiza kabisa, wala hakuwatupa mpaka siku hizo waondoke usoni pake. Hazaeli, mfalme wa Washami, alipokufa, mwanawe Benihadadi akawa mfalme mahali pake. Ndipo, Yoasi, mwana wa Yoahazi, alipoichukua tena ile miji mkononi mwa Benihadadi, mwana wa Hazaeli, baba yake aliyoichukua vitani mkononi mwa Yoahazi. Yoasi alipokwisha kumpiga mara tatu, alikuwa ameirudisha ile miji ya Waisiraeli. Katika mwaka wa 2 wa Yoasi, mwana wa Yoahazi, mfalme wa Waisiraeli, Amasia, mwana wa Yoasi, akapata kuwa mfalme wa Wayuda. Alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 29. Jina la mama yake ni Yoadani wa Yerusalemu. Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana, lakini hakuwa kama baba yake Dawidi; naye akayafanya yote, baba yake Yoasi aliyoyafanya. Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, maana watu waliendelea bado kutambika na kuvukiza vilimani pa kutambikia. Ikawa, ufalme ulipopata kushupaa mkononi mwake, akawaua watumishi wake waliomwua baba yake mfalme. Lakini wana wao wale wauaji hakuwaua, kwa kuwa imeandikwa katika kitabu cha Maonyo ya Mose, Bwana aliyomwagiza kwamba: Baba wasiuawe kwa ajili ya wana, wala wana wasiuawe kwa ajili ya baba, ila kila mtu na auawe kwa kosa lake yeye! Naye ndiye aliyewapiga Waedomu watu 10000 katika Bonde la Chumvi, akauteka nao mji wa Sela katika vita hivyo, akauita jina lake Yokiteli mpaka siku hii ya leo. Kisha Amasia akatuma wajumbe kwa Yoasi, mwana wa Yoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Waisiraeli, kumwambia: Njoo, tuonane uso kwa uso! Naye Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, akatuma wajumbe kwa Amasia, mfalme wa Wayuda, kwamba: Kingugi kilichoko Libanoni kilituma kwa mwangati ulioko Libanoni kwamba: Mpe mwanangu mwanao wa kike, awe mkewe! Ndipo, nyama wa porini wa huko Libanoni alipopita, akakikanyaga kile kingugi na kukiponda. Kwa kuwa umewapiga Waedomu, moyo wako unakukuza; jitutumue, lakini kaa nyumbani mwako! Mbona unataka kujitia katika vita vibaya, uanguke wewe na Wayuda pamoja nawe? Lakini Amasia hakusikia; ndipo, Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, alipopanda, wakaonana uso kwa uso, yeye na Amasia, mfalme wa Wayuda, huko Beti-Semesi katika nchi ya Wayuda. Wayuda wakashindwa na Waisiraeli, wakakimbia kila mtu hemani kwake. Naye Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, akamkamata Amasia, mfalme wa Wayuda, aliyekuwa mwana wa Yoasi, mwana wa Yoahazi, kule Beti-Semesi, kisha akaja Yerusalemu, akalivunja boma la Yerusalemu toka lango la Efuraimu hata lango la pembeni, ndio mikono 400. Akachukua dhahabu na fedha zote, navyo vyombo vyote vilivyopatikana Nyumbani mwa Bwana namo katika vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme nao watu, aliowataka kuwa kole, kisha akarudi Samaria. Mambo mengine ya Yoasi aliyoyafanya na matendo yake yenye nguvu aliyoyatenda alipopiga vita na Amasia, mfalme wa Wayuda, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Yoasi alipokwenda kulala na baba zake, akazikwa Samaria kwa wafalme wa Waisiraeli, naye mwanawe Yeroboamu akawa mfalme mahali pake. Naye Amasia, mwana wa Yoasi, mfalme wa Wayuda, akawapo tena miaka 15 baada ya kufa kwa Yoasi, mwana wa Yoahazi, mfalme wa Waisiraeli. Mambo mengine ya Amasia hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Walipomlia njama mle Yerusalemu, akakimbilia Lakisi; ndipo, walipotuma watu kumfuata huko Lakisi, wakamwua huko. Wakamchukua kwa farasi, akazikwa mle Yerusalemu kwa baba zake mjini mwa Dawidi. Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria aliyekuwa mwenye miaka 16, wakamfanya kuwa mfalme mahali pa baba yake Amasia. Yeye akaujenga Elati, akaurudisha kwao Wayuda, mfalme alipokuwa amelala na baba zake. Katika mwaka wa 15 wa Amasia, mwana wa Yoasi, mfalme wa Wayuda, Yeroboamu, mwana wa Yoasi, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 41. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, hakuyaepuka makosa yote ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli. Yeye akairudisha mipaka ya Waisiraeli toka Hamati mpaka kwenye bahari ya nyikani, kama Bwana Mungu wa Isiraeli alivyosema kinywani mwa mtumishi wake mfumbuaji Yona, mwana wa Amitai, wa Gati-Heferi. Kwani Bwana aliyaona mateso ya Waisiraeli yaliyokuwa yenye machungu sana, akaona, ya kuwa waliofungwa nao waliofunguliwa wanamalizika, kwa kuwa hakuwako aliyewasaidia Waisiraeli. Naye Bwana alikuwa hajasema, ya kuwa atalifuta jina la Isiraeli, litoweke chini ya mbingu, kwa hiyo akawasaidia kwa mkono wa Yeroboamu, mwana wa Yoasi. Mambo mengine ya Yeroboamu, nayo yote, aliyoyafanya, na matendo yake yaliyokuwa yenye nguvu, alipopiga vita, tena jinsi alivyoirudisha kwa Waisiraeli miji ya Damasko na ya Hamati iliyokuwa kale ya Wayuda, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Yeroboamu alipokwenda kulala na baba zake wafalme wa Waisiraeli, mwanawe Zakaria akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 27 wa Yeroboamu, mfalme wa Waisiraeli, Azaria, mwana wa Amasia, akapata kuwa mfalme wa Wayuda. Alikuwa mwenye miaka 16 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 52. Jina la mama yake ni Yekolia wa Yerusalemu. Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama yote, baba yake Amasia aliyoyafanya. Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, maana watu waliendelea bado kutambika na kuvukiza vilimani pa kutambikia. Bwana akampiga mfalme, akawa mwenye ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya wagonjwa waliotengwa, naye mwanawe Yotamu akawa mkuu nyumbani mwa mfalme, akawaamua watu wa nchi hii. Mambo mengine ya Azaria nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Azaria alipokwenda kulala na baba zake, wakamzika kwa baba zake mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Yotamu akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 38 wa Azaria, mfalme wa Wayuda, Zakaria, mwana wa Yeroboamu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miezi 6. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, kama baba zake walivyofanya, hakuyaepuka makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli. Salumu, mwana wa Yabesi, akamlia njama, akampiga machoni pa watu, akamwua, akawa mfalme mahali pake. Mambo mengine ya Zakaria tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli. Hapo limetimia lile neno la Bwana, alilomwambia Yehu kwamba: Wanao wa vizazi vinne watakaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli. Ikawa hivyo. Salumu, mwana wa Yabesi, akapata kuwa mfalme katika mwaka wa 39 wa Uzia, mfalme wa Wayuda, akawa mfalme mle Samaria siku za mwezi mmoja. Ndipo, Menahemu, mwana wa Gadi, wa Tirsa, alipopanda, akaingia Samaria, akampiga Salumu, mwana wa Yabesi, mle Samaria, akamwua, akawa mfalme mahali pake. Mambo mengine ya Salumu nayo njama yake, aliyomlia mfalme, tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli. Siku zile Menahemu akaupiga mji wa Tifusa nao wote waliokuwamo na mipakani kwake toka Tirsa; kwa kuwa hawakumfungulia lango la mji, akawaua, nao wanawake waliokuwa wenye mimba akawatumbua. Katika mwaka wa 39 wa Azaria, mfalme wa Wayuda, Menahemu, mwana wa Gadi, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 10. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, siku zake zote hakuyaepuka makosa yote ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli. Puli, mfalme wa Asuri, alipijia nchi hiyo, ndipo, Menahemu alipompa Puli vipande vya fedha 1000, ndio shilingi milioni 12, kusudi amsaidie kwa mikono yake kuushupaza ufalme wake mkononi mwake. Kisha Menahemu akawatoza Waisiraeli hizo fedha kwa kwamba: Kwao wenye mali kila mmoja ampe mfalme wa Asuri vipande vidogo vya fedha 50, ndio shilingi 200. Kisha mfalme wa Asuri akarudi, hakukaa huko katika nchi hiyo. Mambo mengine ya Menahemu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli? Menahemu alipokwenda kulala na baba zake, mwanawe Pekaya akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 50 wa Azaria, mfalme wa Wayuda, Pekaya, mwana wa Menahemu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 2. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, hakuyaepuka makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli. Peka, mwana wa Remalia, mkuu wake wa askari 30 akamlia njama, akamwua pamoja na Argobu na Arie huko Samaria katika jumba kubwa lililokuwa nyumba ya mfalme, hata watu 50 wa wana wa Gileadi walikuwa naye. Alipokwisha kumwua akawa mfalme mahali pake. Mambo mengine ya Pekaya nayo yote, aliyoyafanya, tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli. Katika mwaka wa 52 wa Azaria, mfalme wa Wayuda, Peka, mwana wa Remalia, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 20. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, hakuyaepuka makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli. Siku za Peka, mfalme wa Waisiraeli, akaja Tiglati-Pileseri, mfalme wa Asuri, akaiteka miji ya Iyoni na Abeli-Beti-Maka na Yanoa na Kedesi na Hasori na Gileadi na Galila, ndiyo nchi yote ya Nafutali, nao watu akawahamisha kwenda Asuri. Ndipo, Hosea, mwana wa Ela, alipomlia njama Peka, mwana wa Remalia, akampiga, akamwua, kisha akawa mfalme mahali pake katika mwaka wa 20 wa Yotamu, mwana wa Uzia. Mambo mengine ya Peka nayo yote, aliyoyafanya, tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli. Katika mwaka wa 2 wa Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Waisiraeli, Yotamu, mwana wa Uzia, mfalme wa Wayuda, akapata kuwa mfalme. Alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 16. Jina la mama yake ni Yerusa, binti Sadoki. Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama yote, baba yake Uzia aliyoyafanya. Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, maana watu waliendelea bado kutambika na kuvukiza vilimani pa kutambikia. Yeye ndiye aliyelijenga lango la juu la Nyumba ya Bwana. Mambo mengine ya Yotamu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Siku zile Bwana akaanza kumtuma Resini, mfalme wa Ushami, na Peka, mwana wa Remalia, waijie nchi ya Yuda. Yotamu alipokwenda kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa baba yake Dawidi, naye mwanawe Ahazi akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 17 wa Peka, mwana wa Remalia, Ahazi, mwana wa Yotamu, mfalme wa Wayuda, akapata kuwa mfalme. Ahazi alikuwa mwenye miaka 20 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 16. Hakuyafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama baba yake Dawidi, ila akaendelea kuzishika njia za wafalme wa Waisiraeli, hata mwanawe akamtumia kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa motoni akiyafuata hayo matapisho ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele yao Waisiraeli. Akatambika na kuvukiza vilimani pa kutambikia napo pengine palipoinukia juu, hata chini yake kila mti uliokuwa wenye majani mengi. Hapo Resini, mfalme wa Ushami, na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Waisiraeli, wakaupandia Yerusalemu kupiga vita, wakamsonga Ahazi kwa kumzinga, lakini hawakuweza kumshinda vitani. Wakati huo Resini, mfalme wa Ushami, akaurudisha mji wa Elati kwa Washami, nao Wayuda akawafukuza mle Elati; ndipo, washami wlipokuja kukaa Elati, wakakaa humo mpaka siku hii ya leo. Ahazi akatuma wajumbe kwa Tiglati-Pileseri, mfalme wa Asuri, kumwambia: Mimi ni mtumwa wako na mtoto wako; panda, uniokoe mkononi mwa mfalme wa Ushami namo mkononi mwa mfalme wa Waisiraeli walioniinukia! Ahazi akazichukua fedha na dhahabu zilizopatikana Nyumbani mwa Bwana namo katika vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme, akazituma kwa mfalme wa Asuri kuwa matunzo. Mfalme wa Asuri akamwitikia; kisha mfalme wa Asuri akaupandia mji wa Damasko, akauteka, nao watu akawahamisha kwenda Kiri, lakini Resini akamwua. Mfalme Ahazi akaenda Damasko kuonana na Tiglati-Pileseri, mfalme wa Asuri. Alipoiona meza ya kutambikia iliyoko Damasko mfalme Ahazi akatuma mfano wa hiyo meza ya kutambikia kuionyesha namna yake, ilivyotengenezwa kazi zake zote, akaupeleka kwa mtambikaji Uria. Ndipo, mtambikaji Uria alipojenga kutambikia, pote pawe sawa na ule mfano, mfalme Ahazi alioutuma toka Damasko; ndivyo, mtambikaji Uria alivyovifanya, mfalme Ahazi alipokuwa hajarudi bado toka Damasko. Mfalme aliporudi toka Damasko, mfalme akaiona hiyo meza ya kutambikia; ndipo, mfalme alipoikaribia hiyo meza ya kutambikia, akateketeza juu yake ng'ombe ya tambiko pamoja na kuivukizia na kutoa vilaji vya tambiko, akaimwagia vinywaji vya tambiko nazo damu za ng'ombe za tambiko za shukrani, alizozitoa kuzinyunyizia ile meza ya kutambikia. Nayo ile meza ya shaba ya kutambikia iliyokuwako mbele ya Bwana akaiondoa mahali pake mbele ya Nyumba, isiwe tena katikati ya hiyo meza mpya ya kutambikia na Nyumba ya Bwana, akaiweka upande wa kaskazini wa hiyo meza mpya ya kutambikia. Kisha mfalme Ahazi akamwagiza mtambikaji Uria kwamba: Katika hii meza kubwa utachoma ng'ombe za tambiko za asubuhi na vilaji vya tambiko vya jioni na ng'ombe za tambiko za mfalme na vilaji vyake vya tambiko na ng'ombe za tambiko za watu wote wa nchi hii na vilaji vyao vya tambiko na vinywaji vyao vya tambiko, nazo damu zote za ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima nazo damu za ng'ombe nyingine za tambiko uinyunyizie. Nayo mambo ya ile meza ya shaba ya kutambikia nitayafikiri, yatakavyokuwa. Mtambikaji Uria akayafanya yote, kama mfalme Ahazi alivyomwagiza. Mfalme Ahazi akavivunja navyo vibao vya kufungia vya vile vilingo, akaiondoa nayo ile mitungi ya shaba iliyowekwa humo, nayo bahari ya shaba akaiondoa juu ya zile ng'ombe za shaba zilizokuwa chini yake, akaiweka juu ya mawe yaliyopangwa. Nao ukumbi wa siku ya mapumziko, walioujenga penye Nyumba hiyo, nao mlango wa nje wa kuingilia mfalme akauondoa na kuuweka pengine penye Nyumba hiyo kwa ajili ya mfalme wa Asuri. Mambo mengine ya Ahazi, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Ahazi alipokwenda kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Hizikia akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 12 wa Ahazi, mfalme wa Wayuda, Hosea, mwana wa Ela, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 9. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, lakini hakuzidi kama wafalme waliokuwa mbele yake. Yeye ndiye, Salmaneseri, mfalme wa Asuri, aliyemjia, naye Hosea, hakuwa na budi kumtumikia na kumtolea mahongo. Kisha mfalme wa Asuri akamwona Hosea kuwa mwenye njama mbaya, kwa kuwa alituma wajumbe kwa So, mfalme wa Misri, akaacha kumpelekea mfalme wa Asuri mahongo, aliyoyapeleka mwaka kwa mwaka; ndipo, mfalme wa Asuri alipomfunga na kumtia kifungoni. Kisha mfalme wa Asuri akaipandia hiyo nchi yote akiupandia mji wa Samaria, akausonga kwa kuuzinga miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa Hosea mfalme wa Asuri akauteka mji wa Samaria, akawahamisha Waisiraeli kwenda Asuri, akawakalisha katika miji ya Hala, tena Habori penye mto wa Gozani na katika miji ya Wamedi. Ikawa hivyo, kwa kuwa wana wa Isiraeli walimkosea Bwana Mungu wao aliyewatoa utumwani katika nchi ya Misri mkononi mwa Farao, mfalme wa Misri, lakini wao wakacha miungu mingine. Wakaendelea na kuyafuata maongozi ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Isiraeli, nayo maongozi, wafalme wa Waisiraeli waliyoyatoa. Hivyo wana wa Isiraeli walimkosea Bwana Mungu wao na kufanya mafichoni mambo yasiyopasa kuyafanya, wakijijengea pa kutambikia vilimani katika miji yao yote iliyokuwa yenye minara tu ya kungojea, namo mijini mlimo na maboma. Wakajisimamishia nguzo za kutambikia na miti ya Ashera katika vilima virefu vyote na chini ya kila mti wenye majani mengi, wakavukiza vilimani po pote pa kutambikia kama wamizimu, Bwana aliowaondoa mbele yao. Kweli walifanya mambo mabaya ya kumkasirisha Bwana, wakiitumikia migogo ya kutambikia, naye Bwana alikuwa amewakataza kwamba: Msilifanye jambo hilo! Tena Bwana aliwashuhudia Waisiraeli na Wayuda vinywani mwa wafumbuaji wote na wachunguzaji wote kwamba: Rudini na kuziacha njia zenu mbaya, myaangalie maagizo yangu na maongozi yangu na kuyafuata Maonyo yote, niliyowaagiza baba zenu, niliyoyatuma kwenu vinywani mwa watumishi wangu waliokuwa wafumbuaji. Lakini hawakusikia, ila walizishupaza kosi zao kuwa kama kosi za baba zao wasiomtegemea Bwana Mungu wao. Wakayakataa maongozi yake na Agano lake, aliloliagana na baba zao, nao ushuhuda wake, aliowashuhudia, wakafuata mambo yasiyo na maana wakifanya yaliyo ya bure kabisa, wakawafuata wamizimu waliokaa na kuwazunguka pande zote, naye Bwana alikuwa amewaagiza, wasifanye kama wao. Wakayaacha maagizo yote ya Bwana Mungu wao, wakajitengenezea vinyago viwili vya ndama kwa shaba zilizoyeyushwa, tena wakajitengenezea vinyago vya Ashera, wakaviangukia navyo vikosi vyote vya mbinguni, wakamtumikia hata Baali. Hata wana wao wa kiume na wa kike wakawatumia kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa motoni, wakaagua maaguaji kwa kutabana, wakajiuza katika utumwa wa kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, wamkasirishe. Ndipo, Bwana alipowachafukia sana Waisiraeli, akawaondoa usoni pake, hakusalia mtu, ila shina la Wayuda peke yake. Lakini Wayuda nao hawakuyaangalia maagizo ya Bwana, nao wakaendelea kuyafuata maongozi, Waisiraeli waliyoyatoa. Ndipo, Bwana alipokikataa kizazi chote cha Isiraeli, akawatesa na kuwatia mikononi mwa wanyang'anyi, mpaka akiwatupa, waondoke kabisa usoni pake. Kwani Waisiraeli walipojitenga nao wa mlango wa Dawidi na kumfanya Yeroboamu, mwana wa Nebati, kuwa mfalme wao, Yeroboamu akawahimiza Waisiraeli, wasimfuate Bwana, akawakosesha kosa kubwa mno. Wana wa Isiraeli wakaendelea kuyafanya makosa yote, Yeroboamu aliyoyafanya, hawakuyaepuka, mpaka Bwana akiwaondoa Waisiraeli usoni pake, kama alivyosema vinywani mwa watumishi wake wafumbuaji, akawatoa Waisiraeli katika nchi yao na kuwahamisha kwenda Asuri mpaka siku hii ya leo. Kisha mfalme wa Asuri akatoa watu mle Babeli na Kuta na Awa na Hamati na Sefarwaimu, akawakalisha katika miji ya Samaria mahali pao wana wa Isiraeli, wakaitwaa nchi ya Samaria, iwe yao, wakakaa katika miji yao. Ikawa, walipoanza kukaa huko, hawakumcha Bwana, naye Bwana akatuma simba kwao, wakaua watu wengine wengine. Ndipo, walipotuma kumwambia mfalme wa Asuri kwamba: Wamizimu, uliowahamisha na kuwakalisha katika miji ya Samaria, hawayajui yampasayo Mungu wa nchi hii, kwa sababu hii ametuma simba kwao, nao wakawaua, kwa kuwa hawajui yampasayo Mungu wa nchi hii. Mfalme wa Asuri akaagiza kwamba: Pelekeni huko mmoja wao watambikaji, mliowatoa huko na kuwahamisha! Na aende, akae huko na kuwafundisha yampasayo Mungu wa nchi hiyo. Ndipo, mmoja wao watambikaji, waliowatoa Samaria na kuwahamisha, alipokuja, akakaa Beteli, akawa akiwafundisha njia za kumcha Bwana. Lakini kila kabila moja wakajitengenezea miungu ya kwao, wakaiweka katika zile nyumba, Waisiraeli walizozijenga vilimani za kutambikia mle; kila kabila moja wakafanya hivyo katika miji yao, walimokaa. Watu wa Babeli wakatengeneza vinyago vya Sukoti-Benoti, watu wa Kuta wakatengeneza vinyago vya Nergali, watu wa Hamati wakatengeneza vinyago vya Asima, watu wa Awa wakatengeneza vinyago vya Nibuhazi na vya Tarkati, nao wa Sefarwaimu wakawateketeza wana wao motoni, wawe ng'ombe za tambiko za Adarameleki na za Anameleki, ndiyo miungu yao wa Sefarwaimu. Basi, hivyo walikuwa wakimcha Bwana, lakini wakajipatia miongoni mwao watambikaji wa vilimani, ndio waliowafanyia kazi za kutambika katika nyumba za vilimani. Hivyo walikuwa wenye kumcha Bwana pamoja na kuitumikia miungu ya kwao, kama ilivyowapasa wamizimu wa kwao, walikotolewa na kuhamishwa kuja huku. Hata siku hii ya leo hufanya, kama hizo desturi zao za kwanza zilivyokuwa: hawamchi Bwana kwa kweli, wala hawafanyi kwa kweli, maongozi yao na desturi zao zilivyo, wala hawaishiki njia ya Maonyo na ya maagizo, Bwana aliyowaagiza wana wa Yakobo, aliyempa jina la Isiraeli. Naye Bwana alikuwa amefanya agano nao na kuwaagiza kwamba: Msiche miungu mingine, wala msiiangukie, wala msiitumikie, wala msiitambikie! Ila Bwana aliyewatoa katika nchi ya Misri kwa nguvu kuu za mkono wake, alioukunjua, yeye sharti mmche, mmwangukie na kumtambikia! Nayo maongozi na maamuzi na Maonyo na maagizo, aliyowaandikia ninyi, sharti myaangalie, myafanye siku zote! Msiche kabisa miungu mingine! Wala msilisahau Agano, nililolifanya nanyi, wala msiche miungu mingine! Ila Bwana Mungu wenu sharti mmche! Naye atawaponya mikononi mwa adui zenu wote. Lakini hawakusikia, ila wao wakafanya, kama hizo desturi zao za kwanza zilivyokuwa. Hivyo ndivyo, hao wamizimu walivyomcha Bwana pamoja na kuvitumikia vinyago vyao. Hata wana wao na wana wa wana wao wakayafanya mpaka siku hii ya leo, kama baba zao walivyoyafanya. Katika mwaka wa 3 wa Hosea, mwana wa Ela, mfalme wa Waisiraeli, Hizikia, mwana wa Ahazi, mfalme wa Wayuda, akapata kuwa mfalme. Alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miake 29; jina la mama yake ni Abi, binti Zakaria. Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama yote, baba yake Dawidi aliyoyafanya. Yeye akayakomesha matambiko ya vilimani, akazivunja nguzo za mawe za kutambikia, navyo vinyago vya Ashera akavikatakata, nayo ile nyoka ya shaba, Mose aliyoitengeneza, akaipondaponda, kwani mpaka siku hizo wana wa Isiraeli walikuwa wakiivukizia na kuiita Nehustani (Kinyago cha Shaba). Akamwegemea Bwana Mungu wa Isiraeli; hakuwako mwingine aliyekuwa kama yeye, wala miongoni mwao wafalme waliomfuata, wala miongoni mwao waliomtangulia. Akagandamana na Bwana, hakuacha kabisa kumfuata, akayaangalia maagizo yake Bwana, aliyomwagiza Mose. Bwana akawa naye, akafanikiwa po pote, alipotoka kufanya kitu; naye mfalme wa Asuri akamkataa akiacha kumtii na kumtumikia. Nao Wafilisti akawapiga, hata mji wa Gaza na mipaka yake kutoka kwenye mnara wa walinzi hata mjini mwenye boma. Ikawa katika mwaka wa nne wa mfalme Hizikia, ndio mwaka wa saba wa Hosea, mwana wa Ela, mfalme wa Waisiraeli, ndipo, Salmaneseri, mfalme wa Asuri, alipoupandia mji wa Samaria, akausonga kwa kuuzinga. Akauteka baada ya miaka mitatu katika mwaka wa sita wa Hizikia, ndio mwaka wa tisa wa Hosea, mfalme wa Waisiraeli; ndipo, Samaria ulipotekwa. Kisha mfalme wa Asuri akawahamisha Waisiraeli kwenda Asuri, akawakalisha katika miji ya Hala, tena Habori penye mto wa Gazoni na katika miji ya Wamedi, kwa kuwa hawakuisikia sauti ya Bwana Mungu wao wakalivunja Agano lake, maana yote, Mose, mtumishi wa Bwana, aliyowaagiza, hawakuyasikia, wala hawakuyafanya. Ikawa katika mwaka wa 14 wa mfalme Hizikia, ndipo, Saniheribu, mfalme wa Asuri, alipoipandia miji yote ya Wayuda iliyokuwa na maboma, akaiteka. Naye Hizikia, mfalme wa Wayuda, akatuma Lakisi kwa mfalme wa Asuri kumwambia: Nimekosa, ondoka kwangu! Nayo, utakayonitoza, basi, nitayachukua, nikupe. Naye mfalme wa Asuri akambandikia Hizikia, mfalme wa Wayuda, kutoa vipande 300 vya fedha, ndio shilingi milioni tatu na nusu na vipande 30 vya dhahabu, ndio shilingi milioni sita na nusu. Hizikia akampa fedha zote zilizopatikana Nyumbani mwa Bwana namo katika vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme. Wakati huo Hizikia akayaondoa mabati ya dhahabu penye milango ya Jumba la Bwana, hata penye zile nguzo, alizozifunika kwa mabati ya dhahabu yeye Hizikia, mfalme wa Wayuda, akampa mfalme wa Asuri. Lakini mfalme wa Asuri akamtuma mkuu wa vita na mkuu wa watumishi wa nyumbani na mkuu wa askari, watoke Lakisi kwenda Yerusalemu na kikosi kikubwa, wakaupandia, wakafika Yerusalemu. Walipokwisha kupanda na kufika wakasimama kwenye mfereji wa ziwa la juu katika barabara iendayo Shambani kwa dobi. Walipomwita mfalme, akawatokea Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme, na Sebuna aliyekuwa mwandishi na Yoa, mwana wa Asafu, aliyekuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa. Mkuu wa askari akawaambia: Mwambieni Hizikia: Hivi ndivyo, anavyosema mfalme mkuu, mfalme wa Asuri: Hilo egemeo, unaloliegemea, ndio nini? Unasema maneno ya midomo tu kwamba: Nimekata shauri na kujipa moyo wa kupiga vita. Sasa unamwegemea nani ukinikataa na kuacha kunitii? Tazama, egemeo lako, unaloliegemea, ni Misri, hilo fimbo la utete unyongekao! Mtu akilikongojea, litamwingia kiganjani, limchome. Ndivyo, Farao, mfalme wa Misri, anavyowawia wote wamwegemeao. Mkiniambia: Tunamwegemea Bwana Mungu wetu, basi, yeye siye, ambaye Hizikia aliwakataza watu kumtambikia vilimani pake pa kutambikia, napo penye meza zake za kutambikia, alipowaambia Wayuda na Wayerusalemu: Sharti mmwangukie mbele ya meza hii ya kumtambikia humu Yerusalemu tu? Sasa na upinge na bwana wangu, mfalme wa Asuri: nitakupa farasi 2000, kama wewe unaweza kujipatia watu wa kuwapanda. Usipowapata utawezaje kuuelekeza nyuma uso wa mwenye amri mmoja tu, ijapo awe mdogo katika watumishi wa bwana wangu? Tena unawaegemea Wamisri, kwa kuwa wako na magari na wapanda farasi. Bwana alikuwa hayuko, nilipopapandia sasa mahali hapa, nipaangamize? Bwana ndiye aliyeniambia: Ipandie nchi hii, uiangamize! Ndipo, Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Sebuna na Yoa walipomwambia mkuu wa askari: Sema Kishami na watumishi wako! Kwani tunakisikia; usiseme na sisi Kiyuda masikioni pa watu hawa walioko ukutani! Mkuu wa askari akawajibu: je? Bwana wangu amenituma kwa bwana wako na kwako kuyasema hayo maneno? Siko kwa watu hawa wanaokaa ukutani watakaokula pamoja nanyi mavi yao na kunywa mikojo yao? Kisha mkuu wa askari akatokea, akapaza sauti sana na kusema Kiyuda kwamba: Yasikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Asuri! Ndivyo, mfalme anavyosema: Hizikia asiwadanganye! Kwani hataweza kuwaponya ninyi mkononi mwangu! Wala Hizikia asiwaegemeze Bwana kwamba: Bwana ndiye atakayetuponya, mji huu usitiwe mkononi mwa mfalme wa Asuri! Msimwitikie Hizikia! Kwani hivi ndivyo, mfalme wa Asuri anavyosema: Fanyeni na mimi maagano ya mbaraka, mje kunitokea, mpate kula kila mtu mazao ya mzabibu wake na ya mkuyu wake, mpate kunywa kila mtu maji ya shimo lake mwenyewe, mpaka nitakapokuja, niwachukue kuwapeleka katika nchi iliyo kama nchi yenu. Nayo ni nchi inayojaa ngano na pombe, ni nchi yenye vyakula na mizabibu, tena ni nchi yenye mafuta ya michekele na asali, mpate kuwapo, msife. Msimwitikie Hizikia! Kwani atawapoteza na kusema: Bwana atatuponya. Je? Miungu ya wamizimu iliweza mmoja tu kuiponya nchi yake, isichukuliwe na mfalme wa Asuri? Ilikuwa wapi miungu ya Hamati na ya Arpadi? Ilikuwa wapi miungu ya Sefarwaimu, nayo yao Hena na Iwa? Hata Samaria haikuweza kuiponya, nisiichukue. Katika miungu yote ya nchi hizi ni ipi iliyoweza kuziponya nchi zao, nisizichukue? Basi, Bwana atawezaje kuuponya Yerusalemu,. nisiuchukue? Watu wakanyamaza, hawakumjibu neno, kwani mfalme alikuwa amewaagiza kwamba: msimjibu! Kisha Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme, na Sebuna aliyekuwa mwandishi na Yoa, mwana wa Asafu, aliyekuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa, wakaja kwa Hizikia wenye nguo zilizoraruliwa, wakamsimulia maneno ya mkuu wa askari. Ikawa, mfalme Hizikia alipoyasikia, akazirarua nguo zake, akajifunga gunia, akaingia Nyumbani mwa Bwana. Akamtuma Eliakimu aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme na Sebuna aliyekuwa mwandishi na watambikaji wazee waliokuwa wamejifunga magunia kwenda kwa mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi. Wakamwambia: Hivi ndivyo, Hizikia anavyosema: Siku hii ya leo ni siku ya kusongwa na ya kupatilizwa na ya kutupwa, kwani watoto wamefikisha kuzaliwa, lakini nguvu za kuwazaa haziko. Labda Bwana Mungu wako ameyasikia yale maneno yote ya mkuu wa askari, ambayo bwana wake, mfalme wa Asuri, alimtuma kumbeua Mungu Mwenye uzima kwa kuyasema; Bwana Mungu wako na ampatilizie yale maneno, aliyoyasikia! Nawe na uje kuwaombea waliosalia walioko bado! Wakaja hao watumishi wa mfalme Hizikia kwake Yesaya. Yesaya akawaambia: Mwambieni bwana wenu hivi: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Usiyaogope yale maneno, uliyoyasikia, vijana wa mfalme wa Asuri waliyonitukana nayo! Utaniona, nikimtia roho nyingine, asikie habari, kisha arudi katika nchi ya kwao, nako huko kwao nitamwangusha kwa upanga. Mkuu wa askari aliporudi akamkuta mfalme wa Asuri, akipiga vita Libuna, kwani alisikia, ya kuwa mfalme ameondoka Lakisi. Huko mfalme akasikia habari ya Tirihaka, mfalme wa Nubi, kwamba: Tazama, ametoka kukupelekea vita! Ndipo, alipotuma tena wajumbe kwake Hizikia kwamba: Hivyo mtamwambia Hizikia, mfalme wa Wayuda, mkisema: Asikudanganye Mungu wako, wewe umwegemeaye kwamba: Yerusalemu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Asuri. Kumbuka, uliyoyasikia mwenyewe, wafalme wa Asuri waliyozifanyizia nchi zote wakiziangamiza na kuzitia mwiko wa kuwapo! Nawe utapona? Je? Miungu ya wamizimu iliwaponya, baba zangu walipowamaliza, wale watu wa Gozani na wa Harani na wa Resefu nao wana wa Edeni walioko Tilasari? Yuko wapi mfalme wa Hamati, naye mfalme wa Arpadi, naye mfalme wa mji wa Sefarwaimu, naye wa Hena, naye wa Iwa? Hizikia alipozichukua barua hizo mikononi mwa wajumbe, akazisoma; kisha akapanda kwenda Nyumbani mwa Bwana. Humo Hizikia akazizingua mbele yake Bwana, kisha Hizikia akamlalamikia Bwana akisema: Bwana Mungu wa Isiraeli uyakaliaye Makerubi, wewe ndiwe Mungu peke yako wa nchi zote za kifalme, wewe ndiwe uliyezifanya mbingu na nchi. Bwana, litege sikio lako, usikie! Bwana, yafumbue macho yako, uone! Yasikie haya maneno ya Saniheribu, aliyoyatuma, akubeue uliye Mungu Mwenye uzima! Ni kweli, Bwana, wafalme wa Asuri wamewaangamiza wamizimu na nchi zao, wakaitupa miungu yao motoni, kwani hiyo siyo miungu, ila ni kazi za mikono ya watu, ni miti na mawe tu, kwa hiyo waliweza kuiharibu. Bwana Mungu wetu, tuokoe sasa mkononi mwake! Ndipo, nchi zote za kifalme zitakapojua, ya kuwa wewe Bwana ndiwe Mungu peke yako. Ndipo, Yesaya, mwana wa Amosi, alipotuma kwake Hizikia kumwambia: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli, uliyemlalamikia kwa ajili ya Saniheribu, mfalme wa Asuri: Nimeyasikia. Nalo hili ndilo neno, Bwana alilolisema kwa ajili yake: Mwanamwali binti Sioni, amekubeza na kukufyoza; binti Yerusalemu, amekutingishia kichwa nyuma yako. Ni nani, uliyembeua na kumtukana? Ni nani, uliyempalizia sauti na kuyaelekeza macho yako juu? Ni Mtakatifu wa Isiraeli. Bwana ndiye, uliyembeua vinywani mwa wajumbe wako ukisema: Kwa kuwa magari yangu ni mengi, nimepanda milimani juu huko ndani Libanoni, nikaikata miangati yake mirefu na mivinje yake iliyochaguliwa, nikafika kwake huko juu kileleni, msitu unakokuwa kama shamba lake la miti. Nilipochimba, nikapata maji mageni ya kunywa, tena nikaikausha mito yote ya Misri kwa nyayo za miguu yangu. Je? Hujasikia kwamba: Niliyoyafanya kale, niliyoyalinganisha siku za mbele, sasa nimeyaleta, yatimie; wewe ukawa wa kutowesha miji yenye maboma, iwe machungu ya mawe na mabomoko. Nao waliokaa humo mikono yao ikawa mifupi, wakastuka, wakaingiwa na soni, wakawa kama mapalizi ya shambani au kama ndago za uwandani au kama majani yameayo juu ya kipaa au kama shamba linyaukalo pasipo kuzaa. Ninakujua kukaa kwako na kutoka kwako na kuingia kwako; ninavijua navyo, unavyovikasirikia. Kwa sababu unanikasirikia, majivuno yako yakapanda kuingia masikioni mwangu, nitakutia pete yangu puani mwako, nayo hatamu yangu midomoni mwako, kisha nitakurudisha katika njia ileile, uliyokuja nayo. Hiki kitakuwa kielekezo chako, Hizikia: Mwaka huu mtakula yaliyojipanda yenyewe, mwaka wa pili mtakula yaliyoota mashinani, mwaka wa tatu mmwage mbegu, mvune. Nayo mizabibu mtapanda, myale matunda yao. Ndipo, masao yao waliopona wa mlango wa Yuda watakapotia mizizi chini, kisha watazaa matunda juu. Kwani Yerusalemu yatatokea masao, nako mlimani kwa Sioni watatokea waliopona. Wivu wake Bwana Mwenye vikosi utayafanya hayo. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya mfalme wa Asuri: hatauingia mji huu, wala hatapiga humu mshale, wala hataukaribishia ngao, wala hataujengea boma la kuuzingia. Njia, aliyokuja nayo, ileile atarudi nayo. Lakini humu mjini hatamwingia; ndivyo, asemavyo Bwana. Nitaukingia mji huu, niuokoe kwa ajili yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi. Ikawa usiku uleule, ndipo, alipotokea malaika wa Bwana, akapiga makambini kwa Waasuri watu 185000. Walipoamka asubuhi wakawaona hao wote, ya kuwa wamekufa, ni mizoga tu. Ndipo, Saniheribu, mfalme wa Waasuri, alipoondoka, aende zake, akarudi kwao, akakaa Niniwe. Ikawa, alipoomba nyumbani mwa mungu wake Nisiroki, ndipo, wanawe Adarameleki na Sareseri walipompiga kwa upanga, kisha wakaikimbilia nchi ya Ararati, naye mwanawe Esari-Hadoni akawa mfalme mahali pake. Siku zile Hizikia akaugua, kufa kukamjia karibu. Ndipo, mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi, alipokuja kwake, akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: yaliyo yako yaagizie walio wa mlango wako! Kwani wewe utakufa, hutarudi kuwa mzima tena. Akageuka na kuuelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana kwamba: E Bwana, na uukumbuke mwenendo, nilioufanya mbele yako kwa welekevu, nikayafanya kwa moyo wote mzima yaliyo mema machoni pako. Kisha Hizikia akalia kilio kikubwa. Ikawa, Yesaya alipokuwa hajatokea mjini katikati, ndipo, neno la Bwana lilipomjia kwamba: Rudi kumwambia Hizikia aliye mkuu wao walio ukoo wangu: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa baba yako Dawidi anavyosema: Nimesikia kuomba kwako, nikayaona nayo machozi yako; na nikuponye, kesho kutwa upate kupanda kuingia Nyumbani mwa Bwana. Siku zako nitaziongeza na kukupa tena miaka kumi na mitano. Namo mkononi mwake mfalme wa Asuri nitakuponya, hata mji huu, maana nitaukingia mji huu kwa ajili yangu na kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi. Kisha Yesaya akasema: Leteni andazi la kuyu! Wakalileta, wakalibandikia jipu lake, akapata kupona. Kisha Hizikia akamwambia Yesaya: Kielekezo changu ndicho nini cha kwamba: Bwana ataniponya, kesho kutwa nipande kuingia Nyumbani mwa Bwana? Yesaya akamwambia: Hiki kitakuwa kielekezo chako kitokacho kwa Bwana cha kwamba: Bwana atalifanya neno hili, alilolisema: Unataka nini? Kivuli kiende mbele vipande kumi au kirudi vipande kumi? Hizikia akasema: Ni vyepesi, kivuli kusogea vipande kumi, kwa hiyo nataka, kivuli kirudi nyuma vipande kumi. Mfumbuaji Yesaya akamlilia Bwana, naye akakirudisha kivuli nyuma vipande vile, kilivyokuwa kimevishuka penye saa ya jua ya Ahazi, navyo vilikuwa vipande kumi. Wakati huo Berodaki-Beladani, mwana wa Baladani, mfalme wa Babeli, akatuma barua na matunzo kwake Hizikia, kwani alisikia, ya kuwa Hizikia aliugua. Hizikia akawasikiliza, akawaonyesha nyumba yote ya kuwekea mali zake, mlimo na fedha na dhahabu na manukato na mafuta mazuri, na nyumba ya mata yake nayo yote pia yaliyooneka katika vilimbiko vyake. Hakikuwako kitu, ambacho Hizikia hakuwaonyesha, wala nyumbani mwake, wala katika ufalme wake wote. Kisha mfumbuaji Yesaya akaja kwa mfalme Hizikia, akamwuliza: Waume hao wamesema nini? Wametoka wapi wakija kwako? Hizikia akajibu: Wametoka nchi ya mbali, wametoka Babeli. Akauliza: Wameona nini katika nyumba yako? Hizikia akajibu: Wameyaona yote yaliyomo nyumbani mwangu, hakuna kitu katika vilimbiko vyangu, ambacho sikuwaonyesha. Ndipo, Yesaya alipomwambia Hizikia: Sikia neno la Bwana! Tazama, ziko siku zitakazokuja, ndipo, yote yaliyomo nyumbani mwako, nayo yote, baba zako waliyoyalimbika hata siku hii ya leo, yatakapopelekwa Babeli, hakitasalia hata kimoja; ndivyo, Bwana anavyosema. Namo katika wanao wa kiume waliotoka mwilini mwako, uliowazaa mwenyewe, watachukuliwa wengine, watumikie jumbani mwa mfalme wa Babeli. Hizikia akamwambia Yesaya: Neno la Bwana, ulilolisema, ni jema; kisha akasema moyoni: Je? Sivyo, katika siku zangu utakuwako utengemano wa kweli? Mambo mengine ya Hizikia nayo matendo yake yote ya vitani yaliyokuwa yenye nguvu nayo, aliyoyafanya ya kutengeneza ziwa na mifereji ya kupeleka maji mjini, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Hizikia alipokwenda kulala na baba zake, mwanawe Manase akawa mfalme mahali pake. Manase alikuwa mwenye miaka 12 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 55 mle Yerusalemu, nalo jina la mama yake ni Hefusiba. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kwa kuyafuata matapisho ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Isiraeli. Akavijenga tena vijumba vya kutambikia vilimani, baba yake Hizikia alivyoviangamiza, akaweka nazo meza za kumtambikia Baali, akatengeneza nacho kinyago cha Ashera, kama Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, alivyofanya, akaviangukia navyo vikosi vyote vya mbinguni na kuvitumikia. Namo Nyumbani mwa Bwana akajenga penginepengine pa kutambikia, namo humo ndimo, Bwana alimosema: Yerusalemu ndimo, Jina langu litakamokaa. Katika nyua zote mbili za Nyumba ya Bwana akajenga pa kuvitambikia vikosi vya mbinguni. Hata mwanawe akamtumia kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa motoni, tena akaagulia mawingu, akapiga bao, akatumia nao wakweza mizimu na wapunga pepo, akazidi kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, amkasirishe. Nacho kinyago cha Ashera, alichokitengeneza, akakiweka katika Nyumba ile, Bwana aliyomwambia Dawidi na mwanawe Salomo: Humu Nyumbani namo Yerusalemu, niliouchagua katika mashina yote ya Isiraeli, nitalikalisha Jina langu kale na kale. Sitaikimbiza tena miguu ya Waisiraeli katika nchi hii, niliyowapa baba zao, wakijiangalia tu na kuyafanya yote, niliyowaagiza, na kuyafuata Maonyo, mtumishi wangu Mose aliyowaagiza. Lakini hawakusikia, naye Manase akawaponza kufanya mabaya kuliko wamizimu, Bwana aliowaangamiza mbele ya wana wa Isiraeli. Kisha Bwana akasema vinywani mwa watumishi wake wafumbuaji kwamba: Kwa kuyafanya hayo matapisho Manase, mfalme wa Wayuda, amefanya mabaya kuliko yote, waliyoyafanya Waamori waliokuwako mbele yake, nao Wayuda akawakosesha kwa kuyatambikia magogo yake. Kwa sababu hii Bwana Mungu wa Isiraeli anasema hivi: Mtaniona, nikileta mabaya, yaingie Yerusalemu nako kwa Wayuda, nao watu wote watakaoyasikia masikio yao yote mawili yatawavuma. Nitautandia Yerusalemu kamba ya kupimia iliyoupima Samaria, niweke nayo mizani iliyoupima mlango wa Ahabu, kisha nitausafisha mji wa Yerusalemu, kama mtu anavyosafisha bakuli, kisha hulifudikiza. Nao watakaosalia kwao waliokuwa wangu nitawatupa na kuwatia mikononi mwa adui zao, wanyang'anywe mali zao na kutekwa na adui zao wote, kwa kuwa wameyafanya yaliyo mabaya machoni pangu, wakanikasirisha tangu siku ile, baba zao walipotoka huko Misri, hata siku hii ya leo. Manase akazidi sana kumwaga damu za watu wasiokosa, akaujaza Yerusalemu hizo damu toka upande huu mpaka upande wa pili; tena kosa lake kubwa lilikuwa hilo la kuwakosesha Wayuda, wayafanye yaliyo mabaya machoni pake Bwana. Mambo mengine ya Manase nayo yote, aliyoyafanya, na makosa yake, aliyoyakosa, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Manase alipokwenda kulala na baba zake, akazikwa katika bustani penye nyumba yake, ndio katika bustani ya Uza, naye mwanawe Amoni akawa mfalme mahali pake. Amoni alikuwa mwenye miaka 22 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 2 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Mesulemeti, binti Harusi, wa Yotiba. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, kama baba yake Manase alivyofanya. Akaendelea kuzishika njia zote, alizozishika baba yake, akayatumikia magogo ya kutambikia, baba yake aliyoyatumikia, naye akayaangukia. Akamwacha Bwana Mungu wa baba zake, hakuishika njia ya Bwana. Ndipo, watumishi wa Amoni walipomlia njama, wakamwua mfalme nyumbani mwake. Lakini watu wa nchi hiyo wakawaua wote waliomlia mfalme Amoni njama, kisha hao watu wa nchi hiyo wakamfanya mwanawe Yosia kuwa mfalme mahali pake. Mambo mengine ya Amoni, aliyoyafanya hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Wakamzika kaburini mwake katika bustani ya uza, naye mwanawe Yosia akawa mfalme mahali pake. Yosia alikuwa mwenye miaka 8 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 31 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Yedida, binti Adaya, wa Boskati. Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana, akaendelea na kuzishika njia zote za baba yake Dawidi, hakuziacha na kujiendea, wala kuumeni, wala kushotoni. Ikawa katika mwaka wa 18 wa ufalme wake Yosia, ndipo, mfalme alipomtuma mwandishi Safani, mwana wa Asalia, mwana wa Mesulamu, kwenda Nyumbani mwa Bwana akimwambia: Nenda kwa mtambikaji mkuu Hilkia, azijumlishe fedha zilizoletwa Nyumbani mwa Bwana, walinzi wa vizingiti wanazozikusanya kwa watu. Kisha wazitie mikononi mwa wenye kazi waliowekwa kuzisimamia kazi za Nyumbani mwa Bwana, nao wawape wazifanyao kazi hizo za Nyumbani mwa Bwana za kupatengeneza, Nyumba ilipobomoka, maseremala na mafundi wengine na waashi, tena wazitumie za kununua miti na mawe ya kuchonga ya kuitengeneza hiyo Nyumba. Lakini wakipewa hizo fedha mikononi mwao, zisihesabiwe nao, kwani walifanya kazi zao kwa welekevu. Ndipo, mtambikaji mkuu Hilkia alipomwambia mwandishi Safani: Nimeona kitabu cha Maonyo Nyumbani mwa Bwana. Kisha Hilkia akampa Safani hicho kitabu, akakisoma. Mwandishi Safani akaja kwa mfalme, akampasha mfalme habari na kumwambia: watumishi wako wamezimimina fedha zilizoonekana Nyumbani mwa Bwana, wakazitia mikononi mwao wenye kazi waliowekwa kuisimamia Nyumba ya Bwana. Kisha mwandishi Safani akamsimulia mfalme kwamba: Mtambikaji Hilkia amenipa kitabu; kisha Safani akakisoma mbele ya mfalme. Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya kitabu cha maonyo, akazirarua nguo zake. Kisha mfalme akamwagiza mtambikaji Hilkia na Ahikamu, mwana wa Safani, na Akibori, mwana wa Mikaya, na mwandishi Safani na Asaya aliyekuwa mtumishi wa mfalme kwamba: Nendeni kuniulizia Bwana mimi na ukoo huu na Wayuda wote kwa ajili ya maneno ya hiki kitabu kilichooneka! Kwani makali ya Bwana yenye moto ni makuu, nayo yanatuwakia sisi, kwa kuwa baba zetu hawakuyasikia maneno ya kitabu hiki na kuyafanya yote, tuliyoandikiwa humo. Ndipo, mtambikaji Hilkia na Ahikamu na Akibori na Safani na Asaya walipokwenda kwa mfumbuaji wa kike Hulda, mkewe Salumu, mwana wa Tikwa, mwana wa Harihasi aliyeyaangalia mavazi; naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili, wakasema naye. Akawaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mwambieni yule mtu aliyewatuma kwangu: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikileta mabaya makali hapa, yawapate wenyeji wa hapa, ndiyo yote, kile kitabu kinayoyasema, alichokisoma mfalme wa Wayuda, Kwa kuwa wameniacha, wakavukizia miungu mingine, wanikasirishe kwa matendo yote ya mikono yao; kwa hiyo makali yangu yenye moto yatapawakia mahali hapa, nayo hayatazimika. Naye mfalme wa Wayuda aliyewatuma kumwuliza Bwana mwambieni haya: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Kwa kuwa hapo, ulipoyasikia maneno yale, moyo wako umelegea, ukajinyenyekeza mbele ya Bwana papo hapo, ulipoyasikia, niliyoyasema ya mahali hapa na ya wenyeji wake kwamba: Patakuwa maangamizo na maapizo, basi, kwa kuwa umeyararua mavazi yako na kunililia mimi, mimi nami nimekusikia; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwa sababu hii utaniona, nikikuita, uje kukutana na baba zako; ndipo, utakapopelekwa kulala kaburini mwako na kutengemana, macho yako yasiyaone hayo mabaya yote, mimi nitakayopaletea mahali hapa. Kisha wakampelekea mfalme majibu haya. Ndipo, mfalme alipotuma wajumbe, wakusanye kwake wazee wote wa Wayuda na wa Yerusalemu. Kisha mfalme akapanda kwenda Nyumbani mwa Bwana pamoja na Wayuda wote na wenyeji wote wa Yerusalemu na watambikaji na wafumbuaji na watu wote pia, wadogo kwa wakubwa, wakaenda naye, akawasomea masikioni pao maneno yote ya kitabu cha Agano kilichooneka Nyumbani mwa Bwana. Kisha mfalme akaja kusimama penye ile nguzo, akafanya mbele ya Bwana agano la kumfuata Bwana na kuyaangalia maagizo yake na mashuhuda yake na maongozi yake kwa moyo wote na kwa roho yote, ayasimamishe maneno ya Agano hili yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Nao watu wote wakaliitikia agano hili, walishike na kulisimamia. Kisha mfalme akamwagiza mtambikaji mkuu Hilkia na watambikaji wa pili na walinzi wa vizingiti, watoe Jumbani mwa Bwana vyombo vyote vilivyotengenezwa vya kumtambikia Baali na Ashera na vikosi vyote vya mbinguni, wakavichoma moto nje ya Yerusalemu kwenye mashamba ya Kidoroni, nayo majivu yao akayatuma kupelekwa Beteli. Akawakomesha watambikaji wa kimizimu, wafalme wa Wayuda waliowaweka, wavukize vilimani pa kutambikia katika miji ya Wayuda na katika mitaa ya Yerusalemu, ndio waliomvukizia Baali, hata jua na mwezi na nyota zilizoko njiani kwa jua na vikosi vyote vya mbinguni. Nacho kinyago kile cha Ashera akakitoa Nyumbani mwa Bwana na kukipeleka nje ya Yerusalemu kwenye mto wa Kidoroni, akakichoma moto huko kwenye mto wa Kidoroni na kukipondaponda, kiwe mavumbi tu, nayo hayo mavumbi akayatupa kwenye makaburi yao walio watuwatu tu. Navyo vyumba vya wagoni wa Patakatifu vilivyokuwamo Nyumbani mwa Bwana akavibomoa; ndimo, wanawake walimofuma mahema ya Ashera. Nao watambikaji wote akawatoa katika miji ya Wayuda, akavichafua vijumba vya vilimani, hao watambikaji walimovukizia toka Geba mpaka Beri-Seba, navyo vijumba vya kutambikia vilimani vilivyokuwa malangoni upande wa kushoto wa hapo pa kuliingilia lango la Yosua, mkuu wa mji, watu walipoingia mjini, navyo akavibomoa kabisa. Lakini wale watambikaji wa vilimani hawakupata ruhusa kutambika penye meza ya kumtambikia Bwana mle Yerusalemu, wakala tu kwa ndugu zao mikate isiyochachwa. Akapachafua napo Tofeti katika bonde la wana wa Hinomu, mtu asiweze tena kumtolea Moleki mwanawe wa kiume au wa kike, awe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa motoni. Akawakomesha nao wale farasi, wafalme wa Wayuda waliowekea jua hapo pa kuingia Nyumbani mwa Bwana karibu ya chumba cha kulalia cha mtumishi wa nyumbani Natani-Meleki kilichokuwa katika kijumba kile kilichojengwa upande wa machweoni kwa jua, nayo magari ya jua akayateketeza motoni. Nazo meza za kutambikia zilizokuwa darini penye chumba cha juu cha Ahazi zilizotengenezwa na wafalme wa Wayuda nazo meza za kutambikia, Manase alizozitengeneza katika nyua zote mbili za Nyumba ya Bwana, mfalme akazivunjavunja na kuzitoa hapo, kisha akayatupa mavumbi yao katika mto wa Kidoroni. Mfalme akavichafua navyo vijumba vya vilimani pa kutambikia vilivyoko ng'ambo ya Yerusalemu kuumeni kwenye Mlima wa Mwangamizaji, Salomo, mfalme wa Waisiraeli, alivyovijenga vya kutambikia Astoreti, lile tapisho la Wasidoni, na Kemosi, lile tapisho la Wamoabu, na Milkomu, lile chukizo la wana wa amoni. Akazivunja nazo nguzo za mawe za kutambikia, nayo miti ya Ashera akaikatakata, kisha akapajaza mahali pao mifupa ya watu. Akaivunjavunja nayo meza ya kutambikia iliyokuwa Beteli kilimani. Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli, alikotengeneza kijumba cha kutambikia; basi, ile meza yenyewe pamoja na kijumba cha kutambikia pale kilimani akaivunjavunja, kisha yote pia yaliyokuwako huko kilimani akayateketeza kwa moto, akayapondaponda, yawe mavumbi tu, hata kinyago cha Ashera akakiteketeza. Yosia alipogeuka akaona makaburi yaliyokuwa katika mlima ule, akatuma kuichukua mifupa iliyokuwa mle makaburini, akaiteketeza juu ya meza ya kutambikia, akaichafua hivyo kwa lile neno la Bwana, alilolitangaza yule mtu wa Mungu aliyeyatangaza mambo haya. Akauliza tena: Hicho kijengo, ninachokiona, ndio nini? Watu wa huo mji wakamwambia: Ni kaburi la mtu wa Mungu aliyetoka Yuda na kuyatangaza haya, uliyoyafanya juu ya meza ya kutambikia huku Beteli. Ndipo, aliposema: Mwacheni huyu, alale! Mtu asiisumbue mifupa yake! Basi, wakaacha kuigusa mifupa yake nayo mifupa ya mfumbuaji aliyetoka Samaria. Nazo nyumba zote zilizojengwa za kutambikia vilimani kwenye miji ya Samaria, wafalme wa Waisiraeli walizozijenga, wamkasirishe Bwana, Yosia akaziondoa, nazo akazifanyizia mambo kama yale yote, aliyoyafanya huko Beteli. Nao watambikaji wote wa vilimani waliokuwako huko akawachinja, wawe ng'ombe za tambiko juu ya zile meza za kutambikia, hata mifupa ya watu akaiteketeza juu yao, kisha akarudi Yerusalemu. Kisha mfalme akawaagiza watu wote kwamba: Fanyeni sikukuu ya Pasaka ya Bwana, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha Agano! Kwani Pasaka kama hiyo haikufanywa tangu siku za waamuzi waliowaamua Waisiraeli hata siku zote za wafalme wa Waisiraeli na wa Wayuda. Ila Pasaka hii ya Bwana ilifanywa mle Yerusalemu katika mwaka wa 18 wa mfalme Yosia. Nao wakweza mizimu na wapunga pepo na vinyago vya nyumbani na magogo ya kutambikia na matapisho yote yaliyoonekana katika nchi ya Yuda namo Yerusalemu Yosia akayaondoa, kusudi ayatimize maneno ya Maonyo yaliyoandikwa katika kile kitabu, mtambikaji Hilkia alichokiona Nyumbani mwa Bwana. Mfalme kama yeye hakuwako mbele yake aliyemwelekea Bwana kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote na kwa nguvu yake yote, ayafanye Maonyo yote ya Mose, wala nyuma yake hakuondokea aliyekuwa kama yeye. Lakini Bwana hakuyaacha makali yake makuu yenye moto yaliyowawakia Wayuda kwa ajili ya matendo ya kumkasirisha, manase aliyomkasirisha nayo. Kwa hiyo Bwana akasema: Wayuda nao nitawaondoa usoni pangu, kama nilivyowaondoa Waisiraeli, tena nitautupa nao mji huu wa Yerusalemu, niliouchagua, nayo Nyumba hii, niliyoisema: Jina langu litakaa humu. Mambo mengine ya Yosia nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Hizo siku zake akapanda Farao Neko, mfalme wa Misri, kwenda kupigana na mfalme wa Asuri kwenye mto wa Furati. Mfalme Yosia alipotoka kumpinga, yule akamwua kule Megido papo hapo, alipomwona. Watumishi wake wakamchukua garini, alipokwisha kufa, wakamtoa Megido na kumpeleka Yerusalemu, wakamzika kaburini mwake. Kisha watu wa nchi hii wakamchukua Yoahazi, mwana wa Yosia, wakampaka mafuta, wakamfanya kuwa mfalme mahali pa baba yake. Yoahazi alikuwa mwenye miaka 23 alipoupata ufalme, akawa mfalme miezi 3 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Hamutali, binti Yeremia, wa Libuna. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kama yote, baba zake waliyoyafanya. Farao Neko akamfunga huko Ribula katika nchi ya Hamati, asiwe mfalme mle Yerusalemu, akailipisha nchi hii vipande 100 vya fedha, ndio shilingi milioni na 200000, na kipande kimoja cha dhahabu, ndio shilingi 220000. Kisha Farao Neko akamfanya Eliakimu, mwana wa Yosia, kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia, akaligeuza jina lake, akamwita Yoyakimu. Lakini Yoahazi akamchukua, aje naye Misri; ndiko, alikokufa. Zile fedha na dhahabu Yoyakimu akampa Farao; lakini hakuwa na budi kuitoza nchi machango, apate kuzilipa hizo fedha, Farao alizozitaka; watu wa hiyo nchi yake akamtoza kila mmoja kwa mali, alizowaziwa kuwa nazo; ndivyo, alivyowachangisha hizo fedha na dhahabu za kumpa Farao Neko. Yoyakimu alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 11 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Zebuda, binti Pedaya, wa Ruma. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kama yote, baba zake waliyoyafanya. Hizo siku zake Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, akapanda huko; ndipo, Yoyakimu alipomtumikia miaka 3, kisha akamkataa tena akiacha kumtii. Ndipo, Bwana alipotuma kwake vikosi vya Wakasidi na vikosi vya Washami na vikosi vya Wamoabu na vikosi vya wana wa Amoni, akawatuma katika nchi ya Yuda, waiangamize kwa lile neno la Bwana, alilolisema vinywani mwa watumishi wake wafumbuaji. Hivyo vikaingia katika nchi ya Yuda kwa lile neno, kinywa cha Bwana kililolisema, aiondoe usoni pake kwa ajili ya makosa ya Manase, aliyoyafanya yote. Hata kwa ajili ya damu zao wasiokosa, alizozimwaga, akaujaza Yerusalemu hizo damu zao wasiokosa, kwa sababu hii Bwana hakutaka kuwaondolea makosa. Mambo mengine ya Yoyakimu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda? Yoyakimu alipokwenda kulala na baba zake, mwanawe Yoyakini akawa mfalme mahali pake. Lakini mfalme wa Misri hakutoka tena katika nchi yake, kwani mfalme wa Babeli aliichukua nchi yote iliyokuwa yake mfalme wa Misri toka kwenye mto wa Misri mpaka kwenye jito la Furati. Yoyakini alikuwa mwenye miaka 18 alipoupata ufalme, akawa mfalme miezi 3 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Nehusta, binti Elnatani, wa Yerusalemu. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kama yote, baba zake waliyoyafanya. Wakati huo wakapanda watumishi wa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, kwenda Yerusalemu, mji huu ukaja kusongwa kwa kuzingwa. Naye Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, akaja Yerusalemu, watumishi wake walipokuwa wakiusonga huo mji kwa kuuzinga. Ndipo, Yoyakini, mfalme wa Wayuda, alipomtokea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake na watumishi wake na wakuu wake na watumishi wake wa nyumbani, naye mfalme wa Babeli akamchukua katika mwaka wa 8 wa ufalme wake yeye. Akatoa navyo vilimbiko vyote vya Nyumba ya Bwana na vilimbiko vya nyumba ya mfalme, dhahabu na vyombo vyote, Salomo, mfalme wa Waisiraeli, alivyovitengeneza vya kutumiwa Jumbani mwa Bwana, akavivunjavunja, kama Bwana alivyosema. Akawahamisha Wayerusalemu wote na wakuu wote na mafundi wa vita wenye nguvu, nao walikuwa mateka 10000 na mafundi wote na wahunzi, hakusalia mtu, wasipokuwa watu wanyonge wa nchi hiyo. Naye Yoyakini akamhamisha kwenda Babeli na mamake mfalme na wakeze mfalme na watumishi wake wa nyumbani, nao wenye macheo katika nchi hii akawatoa Yerusalemu na kuwapeleka Babeli kifungoni. Tena wenye nguvu wote 7000, na mafundi na wahunzi 1000, wote ni mafundi wa kweli wa kupiga vita; hao mfalme wa Babeli akawapeleka Babeli kifungoni. Kisha mfalme wa Babeli akamfanya baba yake mdogo Matania kuwa mfalme mahali pake, akaligeuza jina lake, akamwita Sedekia. Sedekia alikuwa mwenye miaka 21 alipoupata ufalme; akawa mfalme miaka 11 mle Yerusalemu; jina la mama yake ni Hamutali, binti Yeremia, wa Libuna. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kama yote, Yoyakimu aliyoyafanya. Kwani ikawa kwa ajili ya makali ya Bwana yaliyouwakia mji wa Yerusalemu, hata nchi ya Yuda, akiwatupa, waondoke usoni pake. Kisha Sedekia akamkataa mfalme wa Babeli akiacha kumtii. Ikawa katika mwaka wa 9 wa ufalme wake katika mwezi wa kumi siku ya kumi ya mwezi, ndipo, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alipoujia Yerusalemu yeye na vikosi vyake vyote, wakapiga makambi huko, wakaujengea boma la kuuzungusha. Mji ukaja kusongwa hivyo na kuzingwa mpaka mwaka wa 11 wa mfalme Sedekia. Siku ya tisa ya mwezi wa nne njaa ikazidi mle mjini, watu wa nchi hii hawakuwa na vyakula. Ndipo, mji ulipobomolewa, nao wapiga vita wote wakatoroka usiku huo kwa njia ya lango lililokuwa kati ya kuta mbili penye bustani ya mfalme, nao Wakasidi walikuwa wamelala na kuuzunguka mji, wale wakishika njia ya nyikani. Kisha vikosi vya Wakasidi vikamfuata mfalme na kupiga mbio, vikampata katika nyika ya Yeriko, navyo vikosi vyake vyote vilikuwa vimetawanyika na kumwacha. Wakamkamata mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribula, wakasema naye na kumhukumu. Wanawe Sedekia wakawaua machoni pake, kisha wakayapofua macho yake Sedekia, wakamfunga kwa minyororo, wakampeleka Babeli. Katika mwezi wa tano siku ya saba ya mwezi-ulikuwa mwaka wa 19 wa mfalme Nebukadinesari, mfalme wa Babeli-ndipo, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, mtumishi wa mfalme wa Babeli, alipoingia Yerusalemu. Akaiteketeza Nyumba ya Bwana na nyumba ya mfalme, nazo nyumba zote za Yerusalemu, nazo nyumba kubwa zote akaziteketeza kwa moto. Kisha vikosi vyote vya Wakasidi waliokuwa na mkuu wao waliomlinda mfalme vikazibomoa kuta za boma lililouzunguka Yerusalemu. Masao ya watu waliosalia mjini nao waliokuwa wamemwangukia mfalme wa Babeli na kurudi upande wake, hayo masao yote ya mtutumo wa watu Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawateka na kuwahamisha. Lakini wanyonge wa nchi hii mkuu wao waliomlinda mfalme akawasaza, wengine waiangalie mizabibu, wengine walime tu. Lakini zile nguzo mbili za shaba zilizokuwa penye Nyumba ya Bwana na vile vilingo vya kuwekea mitungi ya maji na bahari ya shaba iliyokuwa penye Nyumba ya Bwana Wakasidi wakazivunja, nazo zile shaba zao wakazipeleka Babeli. Hata masufuria na majembe na makato ya kusafishia mishumaa na kata navyo vyombo vyote pia vya shaba vilivyotumiwa Nyumbani mwa Bwana wakavichukua. Nazo sinia na vyano vilivyokuwa vya dhahabu tupu navyo vilivyokuwa vya fedha tupu, mkuu wao waliomlinda mfalme akavichukua. Zile nguzo mbili na ile bahari moja na vile vilingo vya kuwekea mitungi ya maji, ambavyo mfalme Salomo alivitengenezea Nyumba ya Bwana, shaba zao hivi vyombo vyote hazikuwezekana kupimwa kwa mizani. Nguzo moja urefu wake ulikuwa mikono kumi na nane, juu yake palikuwa na kilemba cha shaba, urefu wa kwenda juu wa hicho kilemba ulikuwa mikono mitatu; hicho kilemba kilikuwa kimezungukwa na misuko kama ya mkeka iliyokuwa yenye komamanga, yote pia ni ya shaba; nayo nguzo ya pili ilikuwa vivyo hivyo, nayo ilikuwa yenye misuko kama ya mkeka. Mkuu wao waliomlinda mfalme akamchukua mtambikaji mkuu Seraya na mtambikaji wa pili Sefania nao walinda kizingiti watatu. Namo mjini akachukua mtumishi mmoja wa nyumbani mwa mfalme aliyewekwa kuwa mkuu wa kuwasimamia wapiga vita na watu watano waliokuwa na kazi machoni pa mfalme waliopatikana mjini na mwandishi wa mkuu wa vikosi aliyewaandika watu wa nchi waliotakiwa uaskari na watu sitini wa shambani waliopatikana mle mjini. Hao akawachukua Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawapeleka Ribula kwa mfalme wa Babeli. Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribula katika nchi ya Hamati. Kisha akwahamisha Wayuda, waitoke nchi yao. Wale watu waliosalia katika nchi ya Yuda, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, aliowasaza, akawawekea Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Safani, kuwasimamia. Wakuu wote wa vikosi, wao na watu wao, waliposikia, ya kuwa mfalme wa Babeli amemweka Gedalia kuwasimamia, wakaja Misipa kwa Gedalia; ndio Isimaeli, mwana wa Netania, na Yohana, mwana wa Karea, na Seraya, mwana wa Tanumeti, wa Netofa, na Yazania, mwana wa mtu wa Maka, hao wenyewe na watu wao. Waume hawa na watu wao Gedalia akawaapia na kuwaambia: Msiwaogope watumishi wa Wakasidi! Kaeni katika nchi hii na kumtumikia mfalme wa Babeli! Ndipo, mtakapoona mema. Ikawa katika mwezi wa saba, ndipo, Isimaeli, mwana wa Netania, mwana wa Elisama wa kizazi cha kifalme, alipokuja pamoja na watu kumi, wakampiga Gedalia, naye kafa; wakawaua hata Wayuda na Wakasidi waliokuwa naye huko Misipa. Kisha watu wote, wadogo kwa wakubwa, na wakuu wa vikosi wakaondoka, wakaja Misri, kwani waliwaogopa Wakasidi. Ikawa katika mwaka wa 37 wa kuhamishwa kwake Yoyakini, mfalme wa Wayuda, katika mwezi wa kumi na mbili siku ya ishirini na saba, ndipo, Ewili-Merodaki, mfalme wa Babeli, alipomwonea uchungu Yoyakini, mfalme wa Wayuda; ikawa katika mwaka huohuo, alipoupata ufalme, akamtoa kifungoni, akasema naye maneno mema, akampa kiti chake cha kifalme juu ya viti vya wafalme wengine waliokuwa naye huko Babeli. Ndipo, alipoyavua mavazi ya kifungoni, akala chakula usoni pa mfalme pasipo kukoma siku zote, alizokuwapo. Nazo mali za kujitunza kila siku akapewa na mfalme wa Babeli, siku kwa siku akapata yaliyompasa siku zote, alizokuwapo. Adamu, Seti, Enosi, Kenani, Mahalaleli, Yaredi, Henoki, Metusela, Lameki, Noa, Semu, Hamu na Yafeti. Wana wa Yafeti: Gomeri na Magogi na Madai na Yawani na Tubali na Meseki na Tirasi. Nao wana wa Gomeri: Askenazi na Rifati na Togarma. Nao wana wa Yawani: Elisa na Tarsisa, Wakiti na Wadodani. Wana wa Hamu: Kusi na Misri, Puti na Kanaani. Nao wana wa Kusi: Seba na Hawila na Sabuta na Rama na Sabuteka. Nao wana wa Rama: Saba na Dedani. Naye Kusi akamzaa Nimurodi; ndiye aliyeanza kuwa mwenye nguvu katika nchi. Naye Misri akawazaa Waludi na Waanami na Walehabi na Wanafutuhi na Wapatirusi na Wakasiluhi, ambao Wafilisti walitoka kwao, na Wakafutori. Naye Kanaani akamzaa Sidoni, mwanawe wa kwanza, na Hiti; tena Myebusi na Mwamori na Mgirgasi, na Mhiwi na Mwarki na Msini, na Mwarwadi na Msemari na Mhamati. Wana wa Semu: Elamu na Asuri na Arpakisadi na Ludi na Aramu na Usi na Huli na Geteri na Meseki. Naye Arpakisadi akamzaa Sela, naye Sela akamzaa Eberi. Naye Eberi akazaliwa wana wawili: jina lake wa kwanza ni Pelegi (Gawanyiko), kwa kuwa siku zake ndipo, nchi hii ilipogawanyika; nalo jina la nduguye ni Yokitani. Naye Yokitani akamzaa Almodadi na Selefu na Hasarmaweti na Yera, na Hadoramu na Uzali na Dikla, na Ebali na Abimaeli na Saba, na Ofiri na Hawila na Yobabu; hawa wote ndio wana wa Yokitani. Semu, Arpakisadi, Sela, Eberi, Pelegi, Reu, Serugi, Nahori, Tera, Aburamu naye ndiye Aburahamu. Wana wa Aburahamu ni Isaka na Isimaeli. Navyo vizazi vyao ni hivi: Mwanawe wa kwanza wa Isimaeli ni Nebayoti, tena Kedari na Adibeli na Mibusamu, Misima na Duma, Masa, Hadadi na Tema, Yeturi, Nafisi na Kedima. Hawa ndio wana wa Isimaeli. Nao wana wa Ketura, suria yake Aburahamu, ni hawa: Akamzaa Zimurani na Yokisani na Medani na Midiani na Isibaki na Sua. Nao wana wa Yokisani ni Saba na Dedani. Nao wana wa Midiani ni Efa na Eferi na Henoki na Abida na Eldaa. Hawa wote ndio wana wa Ketura. Kisha Aburahamu akamzaa Isaka; nao wana wa Isaka ni Esau na Isiraeli. Wana wa Esau: Elifazi, Reueli na Yeusi na Yalamu na Kora. Wana wa Elifazi: Temani na Omari na Sefi na Gatamu, Kenazi na Timuna na Amaleki. Wana wa Reueli: Nahati, Zera, Sama na Miza. Nao wa Seiri: lotani na Sobali na Siboni na Ana na Disoni na Eseri na Disani. Nao wana wa Lotani: Hori na Homamu, naye umbu lake Lotani ni Timuna. Wana wa Sobali: Aliani na Manahati na Ebali, Sefi na Onamu. Nao wana wa Siboni ni Aya na Ana. Wana na Ana: Disoni, nao wana wa Disoni: Hamurani na Esibani na Itirani na kerani. Wana wa Eseri: Bilihani na Zawani na Yakani. Wana wa Disoni: Usi na Arani. Nao hawa ndio wafalme walioshika ufalme katika nchi ya Edomu, wana wa Isiraeli walipokuwa hawajapata bado mfalme: Bela, mwana wa Beori; nalo jina la mji wake ni Dinihaba. Bela alipokufa, Yobabu, mwana wa Zera aliyetoka Bosira, akawa mfalme mahali pake. Yobabu alipokufa, Husamu wa nchi ya Watemani akawa mfalme mahali pake. Husamu alipokufa, Hadadi, mwana wa Bedadi aliyewapiga Wamidiani katika mbuga za Wamoabu, akawa mfalme mahali pake; nalo jina la mji wake ni Awiti. Hadadi alipokufa, Samula aliyetoka Masireka akawa mfalme mahali pake. Samula alipokufa, Sauli aliyetoka Rehoboti wa Mtoni akawa mfalme mahali pake. Sauli alipokufa, Baali-Hanani, mwana wa Akibori, akawa mfalme mahali pake. Baali-Hanani alipokufa, Hadadi akawa mfalme mahali pake, nalo jina la mji wake ni Pai; nalo jina la mkewe ni Mehetabeli, binti Matiredi, binti Mezahabu. Hadadi alipokufa, wakawa majumbe wa Edomu jumbe Timuna, jumbe Alia, jumbe Yeteti, jumbe Oholibama, jumbe Ela, jumbe Pinoni, jumbe Kenazi, jumbe Temani, jumbe Mibusari, jumbe Magidieli, jumbe Iramu; hawa ndio waliokuwa majumbe wa Edomu. Wana wa Isiraeli ndio hawa: Rubeni, Simeoni, Lawi na Yuda, Isakari na Zebuluni, Dani, Yosefu na Benyamini, Nafutali, Gadi na Aseri. Wana wa Yuda: Eri na Onani na Sela; hawa watatu alizaliwa na Mkanaani binti Sua. Naye Eri, mwanawe wa kwanza wa Yuda, akawa mbaya machoni pa Bwana, kwa hiyo akamwua. Naye mkwewe Tamari akamzalia Peresi na Zera. Hivyo wana wote wa Yuda walikuwa watano. Wana wa Peresi ni Hesironi na Hamuli. Nao wana wa Zera ni Zimuri na Etani na Hemani na Kalkoli na Dara, wao wote ni watano. Nao wana wa Karmi ni Akari aliyewaponza Waisiraeli kwa kuuvunja mwiko wa kuchukua mali. Nao wana wa Etani ni Azaria. Nao wana wa Hesironi, aliozaliwa, ni Yerameli na Ramu na Kelubai. Naye Ramu akamzaa Aminadabu, naye Aminadabu akamzaa Nasoni aliyekuwa mkuu wa wana wa Yuda. Naye Nasoni akamzaa Salma, naye Salma akamzaa Boazi, naye Boazi akamzaa Obedi, naye Obedi akamzaa Isai, naye Isai akamzaa mwanawe wa kwanza Eliabu na wa pili Abinadabu na wa tatu Simea, wa nne Netaneli, wa tano Radai, wa sita Osemu, wa saba Dawidi. Nao maumbu zao ni Seruya na Abigaili. Nao wana wa Seruya ni Abisai na Yoabu na Asa-Eli, hawa watatu. Naye Abigaili akamzaa Amasa, naye babake Amasa ni Mwisimaeli Yeteri. Naye Kalebu, mwana wa Hesironi, akazaa wana naye mkewe Azuba naye Yerioti; nao wanawe huyo ni hawa: Yeseri na Sobabu na Ardoni. Azuba alipokufa, Kalebu akamchukua Efurati, naye akamzalia Huri. Naye Huri akamzaa Uri, naye Uri akamzaa Besaleli. Halafu Hesironi akaingia kwa binti Makiri, babake Gileadi; naye akamchukua alipokuwa mwenye miaka 60, akamzalia Segubu. Naye Segubu akamzaa Yairi; huyu Yairi akawa mwenye miji 23 katika nchi ya Gileadi. Lakini Wagesuri na Washami wakavichukua vijiji vya Yairi kwao, Kenati na vijiji vyake, vyote pamoja ni miji 60. Hawa wote ni wana wa Makiri, babake Gileadi. Hesironi alipokwisha kufa mle Kalebu-Efurata, ndipo, Abia, mkewe Hesironi, alipomzalia Ashuri, babake Tekoa. Wana wa Yerameli, mwanawe wa kwanza wa Hesironi, walikuwa: wa kwanza Ramu, tena Buna na Oreni na Osemu wa Ahia. Yerameli akawa na mke mwingine, jina lake Atara, naye ni mamake Onamu. Nao wana wa Ramu, mwanawe wa kwanza wa Yerameli, walikuwa: Masi na Yamini na Ekeri. Nao wana wa Onamu walikuwa Samai na Yada; nao wana wa Samai ni Nadabu na Abisuri. Nalo jina la mkewe Abisuri ni Abihaili, naye akamzalia Abani na Molidi. Nao wana wa Nadabu ni Seledi na Apaimu; naye Seledi alipokufa hakuwa na wana. Nao wana wa Apaimu: Isi; nao wana wa Isi: Sesani; nao wana wa Sesani: Alai. Nao wana wa Yada, nduguye Samai: Yeteri na Yonatani; naye Yeteri alipokufa hakuwa na wana. Nao wana wa Yonatani: Peleti na Zaza. Hawa walikuwa wana wa Yerameli. Sesani hakuwa na wana wa kiume, ila wa kike tu. Naye Sesani alikuwa na mtumwa wa Misri, jina lake Yariha. Sesani akamwoza huyo mtumwa wake Yariha mwanawe wa kike, akamzalia Atai. Naye Atai akamzaa Natani, naye Natani akamzaa Zabadi. Naye Zabadi akamzaa Efulali, naye Efulali akamzaa Obedi. Naye Obedi akamzaa Yehu, naye Yehu akamzaa Azaria. Naye Azaria akamzaa Helesi, naye Helesi akamzaa Elasa. Naye Elasa akamzaa Sisimai, naye Sisimai akamzaa salumu. Naye Salumu akamzaa Yekamia, naye Yekamia akamzaa Elisama. Nao wana wa Kalebu, nduguye Yarameli: Mwanawe wa kwanza Mesa aliye babake Zifu, tena wana wa Maresa aliye babake Heburoni. Nao wana wa Heburoni: Kora na Tapua na Rekemu na Sema. Naye Sema akamzaa Rahamu, babake Yorkamu. Naye Rekemu akamzaa Samai. Naye mwana wa Samai ni Maoni; naye Maoni ni babake Beti-Suri. Naye Efa, suria ya Kalebu, akamzaa Harani na Mosa na Gazezi; naye Harani akamzaa Gazezi. Nao wana wa Yadai: Regemu na Yotamu na Gesani na Peleti na Efa na safu. Maka, Suria ya Kalebu, akamzaa Seberi na Tirihana. Tena akamzaa Safu, babake Madimana, na Sewa, babake Makibena, na babake Gibea; naye Akisa ni mwana wa kike wa Kalebu. Hawa walikuwa wana wa Kalebu. Wana wa Huri aliyekuwa mwana wa kwanza wa Efurata ni Sobali, babake Kiriati-Yearimu, na Salma, babake Beti-Lehemu, na Harefu, babake Beti-Gaderi. Nao wana wa sobali, babake Kiriati-Yearimu, walikuwa Haroe, ndio nusu yao wa Menuhoti. Nazo koo za Kiriati-Yearimu ndio Waitiri na Waputi na Wasumati na Wamisirai; kwao hao ndiko, walikotoka Wasorati na Waestauli. Wana wa Salma: Beti-Lehemu na Wanetofati, Atiroti, Beti-Yoabu nayo nusu yao Wamanahati, ndio wasori; nazo koo za waandishi waliokaa Yabesi ndio Watirati, Wasimati, Wasukati. Hawa ndio Wakini waliotoka kwa Hamati, baba yao mlango wa Rekabu. Wana wa Dawidi, aliozaliwa Heburoni, walikuwa hawa: Wa kwanza Amunoni wa Mwizireeli Ahinoamu; wa pili Danieli wa Mkarmeli Abigaili; wa tatu Abisalomu, mwana wa Maka, binti Talmai, mfalme wa Gesuri; wa nne Adonia, mwana wa Hagiti; wa tano Sefatia wa Abitali; wa sita Itiramu wa mkewe Egla. Hawa sita ndio aliozaliwa Heburoni, alimokuwa mfalme miaka saba na miezi sita; lakini Yerusalemu alikuwa mfalme miaka thelatini na mitatu. Namo Yerusalemu alizaliwa hawa: Simea na Sobabu na Natani na Salomo; hawa wanne ni wa Bati-Sua, binti Amieli. Tena Ibuhari na Elisama na Elifeleti na Noga na Nefegi na Yafia na Elisama na Eliada na Elifeleti, ni tisa. Hawa ni wana wote wa wakeze Dawidi pasipo wana wa masuria; naye Tamari alikuwa umbu lao. Naye mwana wa Salomo ni Rehabeamu, mwanawe ni Abia, mwanawe ni Asa, mwanawe ni Yosafati, mwanawe ni Yoramu, mwanawe ni Ahazia, mwanawe ni Yoasi, mwanawe ni Amasia, mwanawe ni Azaria, mwanawe ni Yotamu, mwanawe ni Ahazi, mwanawe ni Hizikia, mwanawe ni Manase, mwanawe ni Amoni, mwanawe ni Yosia. Nao wana wa Yosia: wa kwanza ni Yohana, wa pili Yoyakimu, wa tatu Sedekia, wa nne Salumu. Nao wana wa Yoyakimu ni mwanawe Yekonia, mwanawe ni Sedekia. Nao wana wa Yekonia aliyetekwa ni mwanawe Saltieli, na Malkiramu na Pedaya na Senasari na Yekamia na Hosama na Nedabia. Nao wana wa Pedaya: Zerubabeli na Simei. Nao wana wa Zerubabeli: Mesulamu na Hanania na umbu lao Selomiti; tena Hasuba na Oheli na Berekia na Hasadia na Yusabu-Hesedi, watu watano. Nao wana wa Hanania: Pelatia na Yesaya. Tena wana wa Refaya, wana wa Arnani, wana wa Obadia na wana wa Sekania. Nao wana wa Sekania: Semaya; nao wana wa Semaya: Hatusi na Igali na Baria na Naria na Safati, watu sita. Nao wana wa Naria: Eliyoenai na Hizikia na Azirikamu, watu watatu. Nao wana wa Eliyoenai: Hodawia na Eliasibu na Pelaya na Akubu na Yohana na Delaya na Anani, watu saba. Wana wa Yuda: Peresi, Hesironi na Karmi na Huri na sobali. Naye Raya, mwana wa Sobali, akamzaa Yahati; naye Yahati akamzaa Ahumai na Lahadi. Huu ndio ukoo wao Wasorati. Hawa ndio wana wa babake Etamu: Izireeli na Isima na Idibasi, nalo jina la umbu lao ni Hasilelponi. Tena Penueli, babake Gedori, na Ezeri, babake Husa; hawa ndio wana wa Huri, mwana wa kwanza wa Efurata, babake Beti-Lehemu. Naye Ashuri, babake Tekoa, alikuwa na wanawake wawili: Hela na Nara. Nara akamzalia Ahuzamu na Heferi na Temuni na Ahastari. Hawa ndio wana wa Nara. Nao wana wa Hela: Sereti, Isihari na Etinani. Kosi akamzaa Anubu na Sobeba nao ukoo wa Ahariheli, mwana wa Harumu: Yabesi alikuwa mwenye macheo kuliko ndugu zake, naye mama yake akamwita jina lake Yabesi kwamba: Nimemzaa kwa maumivu. Naye Yabesi akamwomba Mungu wa Isiraeli kwamba: Laiti ungenibariki sana na kuipanua mipaka yangu, mkono wako ukawa pamoja nami, ukanizuilia mabaya, maumivu yasinipate! Mungu akayatimiza aliyoyaomba. Naye Kelubu, ndugu yake Suha, akamzaa Mehiri, ndiye babake Estoni. Naye Estoni akamzaa Beti-Rafa na Pasea na Tehina, babake Iri-Nahasi. Hawa ndio wana waume wa Reka. Nao wana wa Kenazi: otinieli na Seraya; nao wana wa Otinieli: Hatati. Naye Meonotai akamzaa Ofura. Naye Seraya akamzaa Yoabu, babake Ge-Harasimu (Bonde la Wahunzi), kwani walikuwa wahunzi. Nao wana wa Kalebu, mwana wa Yefune: Iru, Ela na Namu; nao wana wa Ela: Kenazi. Nao wana wa Yehaleleli: Zifu na Zifa, Tiria na Asareli. Nao wana wa Ezera: Yeteri na Meredi na Eferi na Yaloni. (Bitia) akachukua mimba ya Miriamu na ya Samai na ya Isiba, babake Estemoa. Naye mkewe wa Kiyuda wa Meredi akamzaa Yeredi, babake Gedori, na Heberi, babake Soko, na Yekutieli, babake Zanoa; lakini wale walikuwa wana wa Bitia, binti Farao, Meredi aliyemchukua, awe mkewe. Nao wana wa mkewe Hodia, umbu lake Nahamu, babake Keila: Mgarmi na Estemoa wa Maka. Nao wana wa Simoni: Amunoni na Rina, Beni-Hanani na Tiloni. Nao wana wa Isi: zoheti na Beni-Zoheti. Wana wa Sela, mwana wa Yuda: Eri, babake Leka, na Lada, babake Maresa, nao ukoo wao waliojua kufuma bafta wa mlango wa Asibea; tena Yokimu na wana waume wa Kozeba na Yoasi na Sarafu waliotawala Moabu, na Yasubi-Lehemu. Lakini maneno haya ni ya kale. Hawa ndio wafinyanzi na wenyeji wa Netaimu na wa Gedera; walikaa huko kwa mfalme na kumfanyia kazi. Wana wa Simeoni: Nemueli na Yamini, Yaribu, Zera, Sauli. Mwanawe alikuwa Salumu, mwanaswe alikuwa Mibusamu, mwanawe alikuwa Misima. Nao wana wa Misima: Mwanawe alikuwa Hamueli, mwanawe alikuwa Zakuri, mwanawe alikuwa Simei. Naye Simei alikuwa mwenye wana wa kiume kumi na sita na wana wa kike sita, lakini ndugu zake hawakuwa na wana wengi, nao ukoo wao wote haukupata watu wengi kama wana wa Yuda. Nao walikaa Beri-Seba na Molada na Hasari-Suali, na Biliha na Esemu na Toladi, na Betueli na Horma na Siklagi, na Beti-Markaboti na Hasari-Susimu na Beti-Biri na Saraimu. Hii ndiyo miji yao, mpaka Dawidi aliposhika ufalme. Navyo vijiji vyao vilikuwa Etamu na Aini, Rimoni na Tokeni na Asani, ni miji mitano. Navyo vijiji vyao vyote vilivyoizunguka miji hii mpaka Baali vilikuwa makao yao, navyo vilikuwa na vitabu vyao vya udugu. Tena: Mesobabu na Yamuleki na Yosa, mwana wa Amasiya, na Yoeli na Yehu, mwana wa Yosibia, mwana wa Seraya, mwana wa Asieli; na Eliyoenai na Yakoba na Yesohaya na Asaya na Adieli na Yesimieli na Benaya, na Ziza, mwana wa Sifi, mwana wa Aloni, mwana wa Yedaya, mwana wa Simuri, mwana wa Semaya. Hawa waliotajwa kwa majina walikuwa wakuu katika ukoo wao, milango ya baba zao ilipokwisha kusambaa kwa wingi. Wakaenda, hata waingie Gedori upande wa maawioni kwa jua wa huko bondeni kuwatafutia mbuzi na kondoo wao malisho. Wakaona malisho mema ya kuwanonesha, nayo ile nchi ilikuwa pana pande zote, tena ilikuwa yenye utulivu na utengemano, kwani kale watu wa Hamu walikuwa wakikaa huko. Wao walioandikwa majina hapo waliingia huko siku zake Hizikia, mfalme wa Yuda, wakayapiga mahema yao pamoja na Wameuni walioonekana huko, wakawatia mwiko wa kuwapo mpaka siku hii ya leo, wakakaa mahali pao, kwani malisho ya mbuzi na kondoo wao yalikuwapo. Nao wengine wao waliokuwa wana wa Simeoni walikwenda milimani kwa Seiri, watu 500, nao wakuu wao walikuwa Pelatia na Naria na Refaya na Uzieli, wana wa Isi. Wakayapiga masao ya Waamaleki walioponea huko, wakakaa huko mpaka siku hii ya leo. Rubeni, mwana wa kwanza wa Isiraeli, alikuwa kweli mzaliwa wake wa kwanza; lakini kwa kuwa aliyachafua malalo ya baba yake, uzaliwa wake wa kwanza walipewa wana wa Yosefu, mwana wa Isiraeli, ingawa hawakuandikiwa uzaliwa wa kwanza katika kitabu cha udugu. Kweli Yuda alikuwa mwenye nguvu katika ndugu zake, naye mtawalaji akatolewa kwake, lakini huo uzaliwa wa kwanza ulikuwa wake Yosefu. Nao wana wa Rubeni, mwana wa kwanza wa Isiraeli, walikuwa: Henoki na Palu, Hesironi na Karmi. Wana wa Yoeli: Mwanawe Semaya, mwanawe huyo Gogi, mwanawe huyo Simei, mwanawe huyo Mika, mwanawe huyo Raya, mwanawe huyo Baali, mwanawe huyo Bera, ambaye Tilgati-Pilneseri, mfalme wa Asuri, alimteka na kumhamisha, maana alikuwa mkuu wa Rubeni. Ndugu zake walioandikwa katika kitabu cha udugu wa koo zao hivyo, walivyofuatana kuzaliwa, mkuu ni Yieli, akafuata Zakaria, tena Bela, mwana wa Azazi, mwana wa Sema, mwana wa Yoeli. Huyu Bela alikaa Aroeri mpaka Nebo na Baali-Meoni. Upande wa maawioni kwa jua alikaa mpaka kufika katika nyika iliyoko kwenye mto wa Furati, kwani makundi yalikuwa mengi katika nchi ya Gileadi. Tena katika siku za Sauli walipiga vita na watu wa Hagri; hao walipokwisha kuuawa kwa mikono yao, wakakaa katika mahema yao upande wote mzima wa maawioni kwa jua wa Gileadi. Nao wana wa Gadi walikaa ng'ambo yao katika nchi ya Basani mpaka Salka. Mkuu alikuwa Yoeli, naye wa pili Safamu, tena Yanai na Safati wa huko Basani. Ndugu zao wa milango ya baba zao: Mikaeli na Mesulamu na Seba na Yorai na Yakani na Zia na Eberi, watu saba. Hawa ndio wana wa Abihaili, mwana wa Huri, mwana wa Yaroa, mwana wa Gileadi, mwana wa Mikaeli, mwana wa Yesisai, mwana wa Yado, mwana wa Buzi. Ahi, mwana wa Abudieli, mwana wa Guni, alikuwa mkuu wa milango ya baba zao. Walikaa Gileadi na Basani na katika vijiji vyao vidogo na katika malisho yote ya Saroni, hata kwenye mipaka yao. Hawa wote waliandikwa katika vitabu vya udugu katika siku za Yotamu, mfalme wa Yuda, na katika siku za Yeroboamu, mfalme wa Isiraeli. Wana wa Rubeni na wa Gadi nao wa nusu ya shina la Manase, wao waliokuwa wenye nguvu, walioweza kushika ngao na panga, waliojua kuvuta pindi, waliofundishwa vita, walikuwa watu 44760; ndio waliotoka kwenda vitani, wakapigana nao Wahagri nao Wayeturi nao Wanafisi nao Wanodabu. Wakasaidiwa kuwashinda, nao Wahagri pamoja nao wote waliokuwa pamoja nao wakatiwa mikononi mwao, kwani walimlilia Mungu katika mapigano, naye akayasikia maombo yao, kwa kuwa walimtegemea. Wakayateka makundi yao: ngamia 50000, mbuzi na kondoo 250000 na punda 2000 na watu 100000. Kwani walioumizwa walianguka wengi, kwa kuwa vita hivyo vilikuwa vimetoka kwake Mungu, wakakaa mahali pao, mpaka walipotekwa na kuhamishwa. Nao wana wa nusu ya shina la Manase walikaa katika nchi hiyo toka Basani mpaka Baali-Hermoni, tena mpaka Seniri na milimani kwa Hermoni, nao walikuwa wengi. Hawa ndio wakuu wa milango ya baba zao. Eferi na Isi na Elieli na Azirieli na Yeremia na Hodawia na Yadieli, nao walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu, watu wenye majina makuu, kwa hiyo walikuwa wakuu wa kweli wa milango ya baba zao. Lakini walipomvunjia Mungu wa baba zao maagano na kufanya ugoni kwa kuifuata miungu ya makabila ya ile nchi, Mungu aliyoyaangamiza mbele yao, ndipo, Mungu wa Isiraeli alipoiamsha roho ya Puli, mfalme wa Asuri, nayo roho yake Tilgati-Pilneseri, mfalme wa Asuri, akawateka na kuwahamisha Warubeni nao Wagadi nao wa nusu ya shina la Manase, akawapeleka Hala na Habori na Hara na mtoni kwa Gozani; ndiko, waliko hata siku hii ya leo. Wana wa Lawi: Gersoni, Kehati na Merari. Nao wana wa Kehati: Amuramu, Isihari na Heburoni na Uzieli. Nao wana wa Amuramu: Haroni na Mose na Miriamu; nao wana wa Haroni: Nadabu na Abihu, Elazari na Itamari. Elazari akamzaa Pinehasi, Pinehasi akamzaa Abisua. Naye Abisua akamzaa Buki, naye Buki akamzaa Uzi. Naye Uzi akamzaa Zeraya, naye Zeraya akamzaa Merayoti. Merayoti akamzaa Amaria, naye Amaria akamzaa Ahitubu. Naye Ahitubu akamzaa Sadoki, naye Sadoki akamzaa Ahimasi. Naye Ahimasi akamzaa Azaria, naye Azaria akamzaa Yohana. Naye Yohana akamzaa Azaria; huyu ndiye aliyekuwa mtambikaji katika Nyumba hiyo, Salomo aliyoijenga Yerusalemu. Azaria akamzaa Amaria, naye Amaria akamzaa Ahitubu. Naye Ahitubu akamzaa Sadoki, naye Sadoki akamzaa Salumu. Naye Salumu akamzaa Hilkia, naye Hilkia akamzaa Azaria. Naye Azaria akamzaa Seraya, naye Seraya akamzaa Yosadaki. Naye Yosadaki ndiye aliyekwenda nao Wayuda na Wayerusalemu, Bwana alipowahamisha kwa mkono wa Nebukadinesari. Wana wa Lawi: Gersomu, Kehati na Merari. Nayo haya ndiyo majina ya wana wa Gersomu: Libuni na Simei. Nao wana wa Kehati: Amuramu na Isihari na Heburoni na Uzieli. Wana wa Merari: Mahali na Musi; huu ndio ukoo wao Walawi kwa milango ya baba zao. Wagersomu: Mwanawe Libuni, mwanawe huyo Yahati, mwanawe huyo Zima, mwanawe huyo Yoa, mwanawe huyo Ido, mwanawe huyo Zera, mwanawe huyo Yatiri. Wana wa Kehati: Mwanawe Aminadabu, mwanawe huyo Kora, mwanawe huyo Asiri, mwanawe huyo Elkana, mwanawe huyo Ebiasafu, mwanawe huyo Asiri, mwanawe huyo Tahati, mwanawe huyo Urieli, mwanawe huyo Uzia, mwanawe huyo Sauli. Nao wana wa Elkana: Amasai na Ahimoti; mwanawe huyo Elkana, wanawe yeye Elkana: mwanawe Sofai, naye mwanawe huyo Nahati, mwanawe huyo Eliabu, mwanawe huyo Yerohamu, mwanawe huyo Elkana, (mwanawe huyo Samweli). Nao wana wa Samweli: Mzaliwa wa kwanza (Yoeli), tena wa pili Abia. Wana wa Merari: Mahali, mwanawe huyo Libuni, mwanawe huyo Simei, mwanawe huyo Uza, mwanawe huyo Simea, mwanawe huyo Hagia, mwanawe huyo Asaya. Hawa ndio, Dawidi aliowaweka kwa ajili ya kuimba Nyumbani mwa Bwana, lile Sanduku lilipokuwa limekwisha kutua. Nao walikuwa wakitumika mbele ya Kao la Hema la Mkutano kwa kuimba, mpaka Salomo alipoijenga Nyumba ya Bwana mle Yerusalemu, wakasimama katika kazi zao na kupokeana zamu kama desturi yao. Nao hao ndio waliosimama katika kazi zao nao wana wao miongoni mwa wana wa Kehati: Mwimbishaji Hemani, mwana wa Yoeli, mwana wa Samweli, mwana wa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elieli, mwana wa Toa, mwana wa Sufu, mwana wa Elkana, mwana wa Mahati, mwana wa Amasai, mwana wa Elkana, mwana wa Yoeli, mwana wa Azaria, mwana wa Sefania, mwana wa Tahati, mwana wa Asiri, mwana wa Ebiasafu, mwana wa Kora, mwana wa Isihari, mwana wa Kehati, mwana wa Lawi, mwana wa Isiraeli. Naye ndugu yake Asafu alisimama kuumeni kwake; Asafu alikuwa mwana wa Berekia, mwana wa Simea, mwana wa Mikaeli, mwana wa Basea, mwana wa Malkia, mwana wa Etini, mwana wa Zera, mwana wa Adaya, mwana wa Etani, mwana wa Zima, mwana wa Simei, mwana wa Yahati, mwana wa Gersomu, mwana wa Lawi. Nako kushotoni walisimama ndugu zao wana wa Merari: Etani, mwana wa Kisi, mwana wa Abudi, mwana wa Maluki, mwana wa Hasabia, mwana wa Amasia, mwana wa Hilkia, mwana wa Amusi, mwana wa Bani, mwana wa Semeri, mwana wa Mahali, mwana wa Musi, mwana wa Merari, mwana wa Lawi. Ndugu zao Walawi wengine walikuwa wamepewa kazi zote za utumishi wa Kao la Nyumba ya Mungu. Naye Haroni na wanawe walikuwa wakivukiza hapo pa kuteketezea ng'ombe za tambiko napo hapo pa kuvukizia, tena walizifanya kazi zote za hapo Patakatifu Penyewe, wawapatie Waisiraeli upozi wakifanya yote, kama Mose, mtumishi wa Mungu, alivyowaagiza. Nao hawa ndio wana wa Aroni: Mwanawe Elazari, mwanawe huyo Pinehasi, mwanawe huyo Abisua, mwanawe huyo Buki, mwanawe huyo Uzi, mwanawe huyo Zeraya, mwanawe huyo Merayoti, mwanawe huyo Amaria, mwanawe huyo Ahitubu, mwanawe huyo Sadoki, mwanawe huyo Ahimasi. Nayo haya ndiyo makao yao, walikotua katika mipaka yao: miongoni mwao wana wa Haroni ukoo wao Wakehati walipatwa na kura ya kwanza, kwa hiyo wakawapa Heburoni katika nchi ya Yuda pamoja na malisho yake yaliyouzunguka. Lakini mashamba ya huo mji na vijiji vyake wakampa Kalebu, mwana wa Yefune. Tena wakawapa wana wa Haroni miji ya kukimbilia ya Heburoni, tena Libuna pamoja na malisho yake na Yatiri na Estemoa pamoja na malisho yake na Hileni pamoja na malisho yake na Debiri pamoja na malisho yake na Asani pamoja na malisho yake na Beti-Semesi pamoja na malisho yake. Tena katika shina la Benyamini Geba pamoja na malisho yake na Alemeti pamoja na malisho yake na Anatoti pamoja na malisho yake. Miji yao yote ilikuwa 13 kwa hesabu ya koo zao. Nao wana wa Kehati waliosalia walipewa miji 10 kwa kupigiwa kura katika ukoo wa hilo shina (Efuraimu), tena katika nusu ya shina la nusu ya Manase. Nao wana wa Gersomu walipewa miji 13, iwe ya ukoo wao katika shina la Isakari na katika shina la Aseri na katika shina la Nafutali na katika shina la Manase huko Basani. Nao wana wa Merari walipewa kwa kupigiwa kura miji 12, iwe ya ukoo wao katika shina la Rubeni na katika shina la Gadi na katika shina la Zebuluni. Ndivyo, wana wa Isiraeli walivyowapa Walawi hiyo miji pamoja na malisho yao. Wakawapa kwa kuipigia kura ile miji, iliyotajwa majina yao katika shina la wana wa Yuda na katika shina la wana wa Simeoni na katika shina la wana wa Benyamini. Nao wengine waliokuwa wa ukoo wa wana wa Kehati walipata miji katika shina la Efuraimu, iwe yao. Wakawapa miji ya kukimbilia ya Sikemu pamoja na malisho yake milimani kwa Efuraimu, tena Gezeri pamoja na malisho yake na Yokimamu pamoja na malisho yake na Beti-Horoni pamoja na malisho yake na Ayaloni pamoja na malisho yake na Gati-Rimoni pamoja na malisho yake. Tena katika nusu ya shina la Manase Aneri pamoja na malisho yake na Bileamu pamoja na malisho yake. Hii ilikuwa yao wengine wa ukoo wa wana wa Kehati waliosalia. Wana wa Gersomu walipata katika ukoo wao wa nusu ya shina la Manase Golani ulioko Basani pamoja na malisho yake na Astaroti pamoja na malisho yake. Tena katika shina la Isakari: Kedesi pamoja na malisho yake na Daberati pamoja na malisho yake na Ramoti pamoja na malisho yake na Anemu pamoja na malisho yake. Tena katika shina la Aseri: Masali pamoja na malisho yake na Abudoni pamoja na malisho yake na Hukoki pamoja na malisho yake na Rehobu pamoja na malisho yake. Tena katika shina la Nafutali: Kedesi wa Galili pamoja na malisho yake na Hamoni pamoja na malisho yake na Kiriataimu pamoja na malisho yake. Wana wa Merari waliosalia walipata katika shina la Zebuluni: Rimoni pamoja na malisho yake na Tabori pamoja na malisho yake; tena ng'ambo ya pili ya Yordani kuelekea Yeriko upande wa Yordani wa maawioni kwa jua katika shina la Rubeni: Beseri wa nyikani pamoja na malisho yake na Yasa pamoja na malisho yake na Kedemoti pamoja na malisho yake na Mefati pamoja na malisho yake. Tena katika shina la Gadi: Ramoti wa Gileadi pamoja na malisho yake na Mahanaimu pamoja na malisho yake na Hesiboni pamoja na malisho yake na Yazeri pamoja na malisho yake. Nao wana wa Isakari: Tola na Pua na Yasubu na Simuroni, ni watu wanne. Nao wana wa Tola: Uzi na Refaya na Yerieli na Yamai na Ibusamu na Samweli, hawa walikuwa vichwa vyao vya milango ya baba zao; wao wa Tola walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu katika vizazi vyao, hesabu yao katika siku za Dawidi ilikuwa watu 22600. Nao wana wa Uzi: Iziraya, nao wana wa Iziraya: Mikaeli na Obadia na Yoeli na Isia, wote pamoja ni wakuu watano. Tena vizazi vya kwao vya milango ya baba zao vilikuwa vyenye vikosi vikubwa vya wapiga vita, watu 36000, kwani walikuwa wenye wanawake na watoto wengi. Nao ndugu zao wa koo zote za Isakari walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu, walioandikwa katika kitabu cha udugu, wote pamoja walikuwa watu 87000. Wa Benyamini: Bela na Bekeri na Yediaeli, watu watatu. Nao wana wa Bela: Esiboni na Uzi na Uzieli na Yerimoti na Iri, vichwa vitano vya milango ya baba zao, nao walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu nyingi; walioandikwa katika kitabu cha udugu walikuwa watu 22034. Wana wa Bekeri: Zemira na Yoasi na Eliezeri na Eliyoenai na Omuri na Yeremoti na Abia na Anatoti na Alemeti; hawa wote walikuwa wana wa Bekeri. Nao vichwa vya milango ya baba zao walioandikwa katika kitabu cha udugu hivyo, walivyofuatana kuzaliwa, walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu, watu 20200. Nao wana wa Yediaeli: Bilihani, nao wana wa Bilihani: Yeusi na Benyamini na Ehudi na Kanaana na Zetani na Tarsisi na Ahisahari. Hawa wote walikuwa wana wa Yediaeli, nao walikuwa vichwa vya milango ya baba zao na mafundi wa vita wenye nguvu nyingi, watu 17200 walioweza kutoka kwenda vitani kupigana. Naye Supimu na Hupimu walikuwa wana wa Iri; tena Husimu na wana wa Aheri. Wana wa Nafutali: Yasieli na Guni na Yeseri na Salumu, ndio wana wa Biliha. Wana wa Manase: Asirieli, aliyemzaa suria yake wa Kishami, ndiye aliyemzaa naye Makiri, babake Gileadi. Naye Makiri akawaoza Hupimu na Supimu, nalo jina la umbu lake ni Maka, nalo jina la mwanawe wa pili ni Selofuhadi, naye Selofuhadi alikuwa na wana wa kike tu. Naye Maka, mkewe Makiri, akazaa mwana wa kiume, akamwita jina lake Peresi, nalo jina la ndugu yake lilikuwa Seresi, nao wanawe ni Ulamu na Rekemu. Nao wana wa Ulamu: Bedani. Hawa ndio wana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase. Umbu lake Hamoleketi akazaa Ishodi na Abiezeri na Mala. Nao wana wa Semida: Ayani na Sekemu na Likihi na Aniamu. Wana wa Efuraimu: Sutela, na mwanawe huyo Beredi, na mwanawe huyo Tahati, na mwanawe huyo Elada, na mwanawe huyo Tahati, na mwanawe huyo Zabadi, na mwanawe huyo Sutela, tena Ezeri na Eladi. Lakini wana wa Gati waliozaliwa katika nchi ile wakawaua, kwa kuwa walishuka kuyachukua makundi yao. Baba yao Efuraimu akawasikitikia siku nyingi, nao ndugu zake wakaja kumtuliza moyo. Kisha akaingia kwake mkewe, akapata mimba, akazaa mwana wa kiume, akamwita jina lake Beria, kwa kuwa mambo mabaya yalikuwa nyumbani mwake. Mwanawe wa kike ni Sera, ndiye aliyejenga Beti-Horoni wa chini na wa juu, tena Uzeni-Sera. Mwanawe ni Refa na Resefu, na mwanawe huyo Tela, na mwanawe huyo Tahani, na mwanawe huyo Ladani, na mwanawe huyo Amihudi, na mwanawe huyo Elisama, na mwanawe huyo Nuni, na mwanawe huyo Yosua. Nchi, waliyoichukua, iwe yao, walikokaa, ni Beteli na vijiji vyake, tena upande wa maawioni kwa jua Narani, na upande wa machweoni kwa jua Gezeri na vijiji vyake na Sekemu na vijiji vyake mpaka Gaza na vijiji vyake. Kando ya mipaka ya wana wa Manase: Beti-Seani na vijiji vyake, Taanaki na vijiji vyake, Megido na vijiji vyake, Dori na vijiji vyake. Humo ndimo, wana wa Yosefu, mwana wa Isiraeli, walimokaa. Wana wa Aseri: Imuna na Isiwa na Iswi na Beria, naye Sera aliyekuwa umbu lao. Nao wana wa Beria: Heberi na Malkieli, huyu ndiye baba yao wa Birzaiti. Heberi akamzaa Yafuleti na Someri na Hotamu, naye umbu lao Sua. Nao wana wa Yafuleti: Pasaki na Bimuhali na Asiwati. Hawa ndio wana wa Yafuleti. Nao wana wa Semeri: Ahi na Roga na Huba na Aramu. Nao wana wa ndugu yake Helemu: Sofa na Imuna na Selesi na Amali. Wana wa Sofa: Sua na Harneferi na Suali na Beri na Imura, Beseri na Hodi na Sama na Silisa na Itirani na Bera. Nao wana wa Yeteri: Yefune na Pisipa na Ara. Nao wana wa Ula: Ara na Hanieli na Risia. Hawa wote walikuwa wana wa Aseri, vichwa vya milango ya baba zao, mafundi wa vita wenye nguvu nyingi waliochaguliwa, wawe vichwa vya wakuu; wao walioandikwa katika kitabu cha udugu kuwa katika vikosi vya wapiga vita hesabu yao ilikuwa watu 26000. Benyamini akamzaa mwanawe wa kwanza Bela, wa pili Asibeli, wa tatu Ahara, wa nne Noha, wa tano Rafa. Wanawe Bela walikuwa: Adari na Gera na Abihudi na Abisua na Namani na Ahoa na Gera na Sefufani na Huramu. Nao hawa ndio wana wa Ehudi; ndio waliokuwa vichwa vya milango ya baba zao waliokaa Geba, waliowahamisha kwenda Manahati: Namani na Ahia na Gera; huyu ndiye aliyewahamisha. Kisha akamzaa Uza na Ahihudi. Saharaimu alizaa katika mashamba ya Wamoabu alipokwisha kuwatuma wakeze Husimu na Baara kwenda zao; kisha akazaa na mkewe Hodesi: Yobabu na Sibia na Mesa na Malkamu na Yeusi na Sakia na Mirma. Hawa ndio wanawe waliokuwa vichwa vya milango ya baba zao. Pamoja na Husimu alikuwa amemzaa Abitubu na Elpali. Nao wana wa Elpali: Eberi na Misamu na Semeri; huyu ndiye aliyejenga Ono na Lodi na vijiji vyake. Naye Beria na Sema ndio waliokuwa vichwa vya milango ya baba zao iliyokaa Ayaloni, walipokwisha kuwafukuza wenyeji wa Gati. Nao ndugu zao ni Sasaki na Yeremoti. Naye Zebadia na Aradi na Ederi na Mikaeli na Isipa na Yoha wlaikuwa wana wa Beria. Naye Zebadia na Mesulamu na Hiziki na Heberi na Isimerai na Izilia na Yobabu walikuwa wana wa Elpali. Naye Yakimu na Zikiri na Zabudi na Elienai na Siltai na Elieli na Adaya na Beraya na Simurati walikuwa wana wa Simei. Naye Isipani na Eberi na Elieli na Abudoni na Zikiri na Hanani na Hanania na Elamu na Anitotia na Ifudia na Penueli walikuwa wana wa Sasaki. Naye Samuserai na Seharia na Atalia na Yaresia na Elia na Zikiri walikuwa wana wa Yerohamu. Hawa ndio vichwa vya milango ya baba zao na wakuu wa vizazi vyao, nao walikaa Yerusalemu. Huko Gibeoni alikaa babake Gibeoni, nalo jina la mkewe ni Maka. Naye mwanawe wa kwanza alikuwa Abudoni, tena Suri na Kisi na Baali na Nadabu na Gedori na Ayo na Zekeri na Mikloti aliyemzaa Simea. Nao hawa walikaa ng'ambo ya ndugu zao kule Yerusalemu kwao ndugu zao. Naye Neri akamzaa Kisi, naye Kisi akamzaa Sauli, naye Sauli akamzaa Yonatani, tena Malkisua na Abinadabu na Esibaali. Naye mwana wa Yonatani alikuwa Meribu-Baali, naye Meribu-Baali akamzaa Mika. Nao wana wa Mika ni Pitoni na Meleki na Tarea na Ahazi. Ahazi akamzaa Yoada, naye Yoada akamzaa Alemeti, tena Azimaweti na Zimuri, naye Zimuri akamzaa Mosa. Naye Mosa akamzaa Bina; mwanawe huyo alikuwa Rafa, mwanawe huyo Elasa, mwanawe huyo Aseli. Naye Aseli alikuwa mwenye wana sita, nayo haya ndiyo majina yao: Azirikamu, Bokeru na Isimaeli na Saria na Obadia na Hanani; hawa wote ndio wana wa Aseli. Nao wana wa ndugu yake Eseki: wa kwanza Ulamu, wa pili Yeusi, wa tatu Elifeleti. Wana wa Ulamu walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu waliojua kuvuta pindi, nao walikuwa wenye wana wa wajukuu wengi, hesabu yao ni 150. Hawa wote walikuwa wana wa wana wa Benyamini. Waisiraeli wote tunawaona, wameandikwa katika kitabu cha udugu, nao hao walioandikwa wamo katika kitabu cha wafalme wa Waisiraeli; lakini Wayuda walihamishwa kwenda Babeli, kwa kuwa walivunja maagano. Nao wa kwanza waliokaa mijini mwao katika nchi ile, waliyoichukua, iwe yao, walikuwa Waisiraeli waliokuwa watuwatu tu na watambikaji na Walawi na watumishi wa Nyumbani mwa Mungu. Waliokaa mle Yerusalemu wengine walikuwa wana wa Yuda, wengine wana wa Benyamani, wengine wana wa Efuraimu, wengine wa Manase. Wayuda: Utai, mwana wa Amihudi, mwana wa Omuri, mwana wa Imuri, mwana wa Bani aliye mmoja wao wana wa Peresi, mwana wa Yuda. Wengine walikuwa Wasiloni: Asaya aliyekuwa mzaliwa wa kwanza pamoja na wanawe, wengine wana wa Zera: Yueli na ndugu zake, wote pamoja ni watu 690. Wengine walikuwa wana wa Benyamini: Salu, mwana wa Mesulamu, mwana wa Hodawia, mwana wa Hasenua; tena Ibunia, mwana wa Yerohamu, na Ela, mwana wa Uzi, mwana wa Mikiri, na Mesulamu, mwana wa Sefatia, mwana wa Reueli, mwana wa Ibunia; tena ndugu zao waliofuata kuzaliwa, watu 956. Watu hawa wote walikuwa vichwa vya milango ya baba zao kwao milango yao. Wengine walikuwa watambikaji: Yedaya na Yoyaribu na Yakini na Azaria, mwana wa Hilkia, mwana wa Mesulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayoti, mwana wa Ahitubu aliyekuwa mkuu Nyumbani mwa Mungu. Tena Adaya, mwana wa Yerohamu, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkia, na Maasai, mwana wa Adieli, mwana wa Yazera, mwana wa Mesulamu, mwana wa Mesilemiti, mwana wa Imeri. Nao ndugu zao waliokuwa vichwa vya milango ya baba zao, watu 1760, nao ni watu walio mafundi wenye nguvu za kufanya kazi za utumishi wa Nyumbani mwa Mungu. Wengine walikuwa Walawi: Semaya, mwana wa Hasubu, mwana wa Azirikamu, mwana wa Hasabia aliyekuwa mmoja wao wana wa Merari. Tena Bakibakari, Heresi na Galali na Matania, mwana wa Mika, mwana wa Zikiri, mwana wa Asafu. Tena Obadia, mwana wa Semaya, mwana wa Galali, mwana wa Yedutuni, na Berekia, mwana wa Asa, mwana wa Elkana aliyekaa katika vijiji vyao Wanetofati. Wangoja malango: Salumu na Akubu na Talmoni na Ahimani pamoja na ndugu zao; naye Salumu alikuwa kichwa chao, naye anashika mpaka leo zamu ya lango la mfalme lililoko upande wa maawioni kwa jua. Hawa ndio walinda malango wa makambi ya wana wa Lawi. Naye Salumu, mwana wa Kore, mwana wa Ebiasafu, mwana wa Kora, na ndugu zake wa mlango wa baba yake wao Wakora, walikuwa wenye kazi za utumishi wa kuwa wangoja vizingiti vya hilo Hema, nao baba zao walikuwa wakingoja pa kuyaingilia makambi ya Bwana. Naye Pinehasi, mwana wa Elazari, alikuwa kale mkuu wao, naye Bwana alikuwa naye. Zakari, mwana wa Meselemia, alikuwa mlinda lango la Hema la Mkutano. Wao wote waliochaguliwa, wawe walinda vizingiti, walikuwa watu 212; nao walikuwa wameandikwa katika kitabu cha udugu katika vijiji vyao; wao ndio, Dawidi na mtazamaji Samweli waliowaweka kwa kuwategemea. Hao wenyewe na wana wao walikuwa wakisimama penye malango ya Nyumba ya Bwana, ile nyumba ya Hema, na kupokeana zamu. Nao hao wangoja malango waliwekwa, waangalie pande zote nne, upepo unakotoka: maawioni kwa jua na machweoni kwa jua, kaskazini na kusini. Nao ndugu zao waliokaa vijijini kwao hawakuwa na budi kufika kila siku ya saba, wapokezane nao zamu kwa zamu. Nao hawa walinda malango walikuwa na wakuu wanne, hao walikaa hapohapo, kwani walitegemewa hivi. Hizi zilikuwa kazi zao Walawi, tena waliwekwa kuviangalia vyumba na vilimbiko vya Nyumbani mwa Mungu. Kwa hiyo walilala usiku pande zote za Nyumba ya Mungu, kwani ilikuwa kazi yao kuiangalia na kuifungua, kila kulipokucha. Wengine wao walikuwa wenye kazi za kuviangalia vyombo vya utumishi, kwani huhesabiwa, walipoviingiza Nyumbani, tena walipovitoa. Wengine wao waliwekwa kuviangalia vyombo vingine, ndio vyombo vyote vilivyomo Patakatifu, nao unga mwembamba nazo mvinyo nayo mafuta nao ubani nayo manukato. Lakini walioyatengeneza mavukizo kwa kuyachanganya hayo manukato walikuwa watambikaji wenyewe. Naye Matitia, mmoja wao Walawi, mwana wa kwanza wa Mkora Salumu, akapewa kuziangalia kazi za kutengeneza maandazi ya tambiko, kwani walimtegemea. Ndugu zao wengine waliokuwa wana wa Kehati wakapewa kuiangalia mikate, aliyowekewa Bwana, waiweke kila siku ya mapumziko. Nao hao ndio waimbaji waliokuwa vichwa vya milango ya baba zao ya Walawi, ndio waliokaa katika vile vyumba, wasiokuwa na kazi nyingine, kwani kazi yao yenyewe iliwataka mchana na usiku. Hawa ndio waliokuwa vichwa vya milango ya baba zao Walawi, maana ni wakuu wa vizazi vyao, nao ndio waliokaa Yerusalemu. Mle Gibeoni alikaa Yieli, babake Gibeoni, nalo jina la mkewe lilikuwa Maka. Mwanawe wa kwanza ni Abudoni, tena Suri na Kisi na Baali na Neri na Nadabu na Gedori na Ayo na Zakaria na Mikloti. Naye Mikloti akamzaa Simeamu. Nao hao walikaa ng'ambo ya ndugu zao kule Yerusalemu kwao ndugu zao. Naye Neri akamzaa Kisi, naye Kisi akamzaa Sauli, naye Sauli akamzaa Yonatani, tena Malkisua na Abinadabu na Esibaali. Naye mwana wa Yonatani alikuwa Meribu-Baali, naye Meribu-Baali akamzaa Mika. Nao wana wa Mika ni Pitoni na Meleki na Tarea na Ahazi. Ahazi akamzaa Yara, naye Yara akamzaa Alemeti, tena Azimaweti na Zimuri, naye Zimuri akamzaa Mosa. Naye Mosa akamzaa Bina, mwanawe huyo alikuwa Refaya, mwanawe huyo Elasa, mwanawe huyo Aseli. Naye Aseli alikuwa mwenye wana sita; nayo haya ndiyo majina yao: Azirikamu, Bokeru na Isimaeli na Saria na Obadia na Hanani; hawa ndio wana wa Aseli. Wafilisti walipopigana nao Waisiraeli, watu wa Isiraeli wakawakimbia Wafilisti kwa madonda waliyopigwa, wakaanguka, wakafa kule mlimani kwa Gilboa. Wafilisti wakawafuata na kuandamana na Sauli na wanawe, Wafilisti wakawaua wana wa Sauli: Yonatani na Abinadabu na Malkisua. Mapigano yakawa makali hapo, Sauli alipokuwa; wapiga mishale walipomwona, akaumizwa nao wapiga mishale. Ndipo, Sauli alipomwambia mchukua mata yake: Uchomoe upanga wako, unichome nao, hao wasiotahiriwa wasije kunichezea vibaya! Mchukua mata yake alipokataa kwa kuogopa sana, Sauli akausimika upanga, akauangukia. Mchukua mata yake alipoona, ya kuwa Sauli amekufa, naye akauangukia upanga wake, akafa. Ndivyo, Sauli alivyokufa na wanawe watatu, nao wa mlango wake wote wakafa pamoja naye. Watu wote wa Isiraeli waliokaa kule katika mbuga ya bondeni walipoona, ya kuwa wamekimbizwa, ya kuwa Sauli na wanawe wamekufa, wakaiacha miji yao wakakimbia nao; kisha Wafilisti wakaja, wakakaa humo. Ikawa kesho yake, Wafilisti walipokuja kuwapambua waliouawa, wakamwona Sauli na wanawe, jinsi walivyokufa mlimani kwa Gilboa. Wakampambua, wakakichukua kichwa chake na mata yake, wakatuma wajumbe kwenda po pote katika nchi ya Wafilisti kuyatangaza penye vinyago vyao, hata kwa watu. Mata yake wakayaweka nyumbani mwa mungu wao, nacho kichwa chake wakakiangika kwa misumari nyumbani mwa Dagoni. Watu wote wa Yabesi wa Gileadi walipoyasikia yote, Wafilisti waliyomfanyizia Sauli, wakaondoka watu wote walioweza kupiga vita, wakauchukua mzoga wa Sauli, nayo mizoga ya wanawe, wakaipeleka Yabesi, wakaizika mifupa yao chini ya mkwaju kwao Yabesi, wakafunga mfungo siku saba. Ndivyo, Sauli alivyokufa kwa kumvunjia Bwana maagano, aliyoyafanya naye, kwa kuwa hakulishika Neno la Bwana, tena kwa kuwa alitafuta mwaguaji aliyejua kukweza mizimu. Kwa kuwa hakutaka kuongozwa na Bwana, akamwua, nao ufalme akauondoa kwake, akampa Dawidi, mwana wa Isai. Waisiraeli wote wakamkusanyikia Dawidi huko Heburoni kumwambia: Tazama, sisi na wewe tu mifupa ya mmoja, nazo nyama za miili yetu ni za mmoja. Napo hapo kale, Sauli alipokuwa mfalme bado, aliyewaongoza Waisiraeli kwenda na kurudi vitani ni wewe, naye Bwana Mungu wako alikuambia: Wewe utawachunga walio ukoo wangu wa Waisiraeli, nawe wewe utawatawala hao walio ukoo wangu wa Waisiraeli. Wazee wote wa Waisiraeli wakamjia mfalme huko Heburoni, Dawidi akafanya agano nao huko Heburoni mbele ya Bwana, wakampaka Dawidi mafuta, awe mfalme wao Waisiraeli, kama Bwana alivyosema kinywani mwa Samweli. Kisha Dawidi na Waisiraeli wote wakaenda Yerusalemu, ndio Yebusi, nao Wayebusi hapo walikuwa bado wenyeji wa nchi hiyo. Nao waliokaa Yebusi wakamwambia Dawidi: Humu hutaingia kabisa! Lakini Dawidi akaliteka boma la Sioni, ndio mji wa Dawidi. Dawidi akasema: Ye yote atakayekuwa wa kwanza wa kuwapiga Wayebusi atakuwa mkuu wa kwanza wa vikosi. Ndipo, Yoabu, mwana wa Seruya, alipopanda wa kwanza, akawa mkuu. Dawidi akakaa mle bomani, kwa hiyo likaitwa mji wa Dawidi. Akaujenga huo mji pande zote za kuuzunguka toka Milo; naye Yoabu akaujenga huo mji kuwa mpya pengine po pote. Dawidi akaendelea kuwa mkuu, kwa sababu Bwana Mwenye vikosi alikuwa naye. Hawa ndio wakuu wao mafundi wa vita, Dawidi aliokuwa nao, waliomsaidia kwa nguvu zao, apate ufalme; nao Waisiraeli wote walikuwa upande wao, walipomfanya kuwa mfalme, kama Bwana alivyowaambia Waisiraeli. Hii ndiyo hesabu yao mafundi wa vita, Dawidi aliokuwa nao: Yasobamu, mwana wa Hakemoni, mkuu wa thelathini; yeye aliuchezesha mkuki wake juu ya watu 300 waliouawa naye kwa mara moja. Aliyemfuata ni Elazari, mwana wa Dodo, wa Ahohi, huyu alikuwa mmoja wao wale mafundi wa vita watatu. Huyu alikuwa pamoja na Dawidi huko Pasi-Damimu, Wafilisti walipokusanyika huko kupigana naye. Huko kulikuwa na kipande cha shamba lenye mawele; hapo, watu walipowakimbia Wafilisti, ndipo, hawa walipokuja kusimama katikati ya hicho kipande cha shamba, wakakiponya wakiwapiga wafilisti; ndivyo, Bwana alivyowaokoa na kuwapatia wokovu mkubwa. Wakashuka wakuu watatu waliomo miongoni mwao wakuu wa thelathini, wafike gengeni kwa Dawidi penye pango la Adulamu; nayo makambi ya Wafilisti yalikuwa Bondeni kwa Majitu. Naye Dawidi siku zile alikuwa ngomeni, nacho kikosi cha walinzi wa Wafilisti kilikuwamo Beti-Lehemu. Hapo Dawidi akaingiwa na tamaa, akasema: Yuko nani atakayeninywesha maji ya kisima cha Beti-Lehemu, kilichoko langoni? Ndipo, wale watatu walipojipenyeza makambini mwa Wafilisti, wakachota maji katika kisima cha Beti-Lehemu kilichoko langoni, wakayachukua, wakamletea Dawidi, lakini Dawidi hakutaka kuyanywa, akammwagia Bwana kuwa kinywaji cha tambiko, akasema: Mungu wangu na anizuie, nisifanye kama hayo! Je? Ninywe damu za waume hawa waliojitoa wenyewe kwa ajili yao haya? Kwani wameyaleta haya kwa kujitoa wenyewe; kwa hiyo hakutaka kuyanywa. Hayo waliyafanya wale mafundi wa vita watatu. Naye Abisai, ndugu yake Yoabu, alikuwa mkuu miongoni mwa watu watatu; yeye ndiye aliyeuchezesha mkuki wake juu ya watu 300, ndio, aliowaua naye; akawa mwenye macheo kwa hao watatu. Kwao hao watatu aliheshimiwa kuliko wenzake wawili, akawa mkuu wao, lakini wale watatu wa kwanza hakuwa sawa nao. Benaya, mwana wa Yoyada, mwana wa mtu mwenye nguvu, alifanya matendo makuu, nako kwao kulikuwa Kabuseli. Yeye aliwaua wana wawili wa Arieli wa Moabu, tena siku moja, theluji ilipokuwa imeanguka, akashuka shimoni, akaua simba mlemle. Naye ndiye aliyemwua mtu wa Misri mwenye urefu wa mikono mitano aliyeshika mkononi mwake mkuki uliokuwa mzito kama majiti ya wafumaji; lakini akamshukia na kushika fimbo tu, akampokonya yule Misri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa huo mkuki wake. Hayo aliyafanya Benaya, mwana wa Yoyada; kwa hiyo alipata macheo kwa hao mafundi wa vita watatu. Kwao hao thelathini aliheshimiwa yeye kuliko wenziwe, lakini wale watatu wa kwanza hakuwa sawa nao. Naye Dawidi akamweka kuwa mkuu wa walinzi wake. Mafundi wa vita wenye nguvu walikuwa hawa: Asaheli, ndugu yake Yoabu; Elihanani, mwana wa Dodo na Beti-Lehemu; Samoti wa Harori, Helesi wa Puloni, Ira, mwana wa Ikesi, wa Tekoa, Abiezeri wa Anatoti, Sibekai wa Husa, Ilai wa Ahohi, Maharai wa Netofa, Heledi, mwana wa Baana, wa Netofa, Itai, mwana wa Ribai, wa Gibea wa wana wa Benyamini, Benaya wa Paratoni, Hurai wa Nahale-Gasi, Abieli wa Araba, Azimaweti wa Bahurimu, Eliaba wa Salaboni, wana wa Hasemu wa Gizoni, Yonatani, mwana wa Sage, wa Harari, Ahiamu, mwana wa Sakari, wa Harari, Elifali, mwana wa Uri, Heferi wa Mekera, Ahia wa Puloni, Hesero wa Karmeli, Narai, mwana wa Ezibai, Yoeli, ndugu yake Natani, Mibuhari, mwana wa Hagri, Mwamoni Seleki, Naharai wa Beroti aliyekuwa mchukua mata wa Yoabu, mwana wa Seruya, Mwitiri Ira, Mwitiri Garebu, Mhiti Uria, Zabadi, mwana wa Alai, Adina, mwana wa Siza, wa Rubeni, aliyekuwa mkuu wao Warubeni mwenye watu 30, Hanani, mwana wa Maka, na Yosafati wa Meteni, Uzia wa Astera, Sama na Yieli, wana wa Hotamu wa Aroeri, Yediaeli, mwana wa Simuri, na nduguye Yoha wa Tisi, Mmahawimu Elieli na Yeribai na Yosawia, wana wa Elinamu, na Mmoabu Itima, Elieli na Obedi na Yasieli wa Soba. Hawa ndio waliomjia Dawidi huko Siklagi, alipokuwa amefukuzwa, asimtokee Sauli, mwana wa Kisi. Nao hao ndio mafundi wa vita waliomsaidia kupigana. Walishika pindi, nao walijua kutupa mawe kuumeni na kushotoni na kupiga mishale kwa pindi zao; nao walikuwa ndugu zake Sauli, maana ni Wabenyamini. Mkuu Ahiezeri na Yoasi, wana wa Hasemaa wa Gibea; na Yezieli na Peleti, wana wa Azimaweti, na Beraka na Yehu wa Anatoti, na Isimaya wa Gibeoni, ni mmoja wao wale mafundi wa vita thelathini, tena ni mkuu wao hao thelathini, na Yeremia na Yahazieli na Yohana na Yozabadi wa Gedera, Eliuzai na Yerimoti na Balia na Semaria na Sefatia wa Harifu; Elkana na Isia na Azareli na Yoezeri na Yasobamu waliokuwa Wakora; na Yoela na Zebadia, wana wa Yerohamu wa Gedori. Kwao Wagadi nako walikuwako waliojitenga kumjia Dawidi kule gengeni nyikani; nao walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu, waume waliozoea kupigana, walishika ngao na mikuki, nyuso zao zilikuwa kama nyuso za simba, wakapiga mbio kama paa milimani. Mkuu Ezeri, wa pili Obadia, wa tatu Eliabu, wa nne Misimana, wa tano Yeremia, wa sita Atai, wa saba Elieli, wa nane Yohana, wa tisa Elizabadi, wa kumi Yeremia, wa kumi na moja Makibanai. Hawa Wagadi walikuwa wakuu wa vikosi, aliyekuwa mdogo kwao aliweza kushinda mia, naye mkubwa elfu. Hawa ndio waliovuka Yordani katika mwezi wa kwanza, mto ulipojaa na kuzifurikia kingo zake zote mbili, wakawafukuza wote waliokaa huko mabondeni upande wa maawioni kwa jua na machweoni kwa jua. Watu wengine wa Benyamini na wa Yuda walipomjia Dawidi pale gengeni pake, Dawidi akawatokea, akaanza kusema nao akiwaambia: Kama mnakuja kwangu kwa kunitakia mema, mnisaidie, basi, moyo wangu utafanya bia nanyi, tupatane; lakini kama mnataka kunichongea kwao wanaonisonga, ingawa ukorofi haumo mikononi mwangu, Mungu wa baba zetu na ayatazame, awapatilize! Ndipo, roho ilipomwingia Amasai aliyekuwa mkuu wa thelathini, akasema: Tu watu wako, Dawidi; tuko pamoja na wewe, mwana wa Isai. Tengemana, tengemana! Naye atakayekusaidia na atengemane! Kwani Mungu wako anakusaidia. Ndipo, Dawidi alipowapokea, akawapa kuwa wakuu wa vikosi. Hata kwa Wamanase walikuwako waliourudia upande wa Dawidi, alipomjia Sauli pamoja na Wafilisti kupigana naye, lakini hawakuwasaidia; kwani wakuu wa Wafilisti walikuwa wamefanya shauri, kwa hiyo walikuwa wamempa ruhusa kwa kumwazia kwamba: Atarudi kwa bwana wake Sauli na kumtolea vichwa vyetu. Kisha alipokwenda Siklagi, Wamanase hawa wakarudi upande wake: Adina na Yozabadi na Yediaeli na Mikaeli na Yozabadi na Elihu na Siltai, ndio wakuu wa vikosi vyenye watu elfu kwao Wamanase. Hawa wakamsaidia Dawidi kushindana na askari za adui, kwani wao wote walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu, wakawa wakuu wa vikosi. Kwani siku hizo watu wakaja kwa Dawidi siku kwa siku, wamsaidie, mpaka wakiwa jeshi kubwa kama jeshi la Mungu. Hii ndiyo hesabu ya wakuu wao wapiga vita waliomjia Dawidi huko Heburoni wakishika mata yao, wampe ufalme wakiuondoa kwake Sauli, kama Bwana alivyosema: wana wa Yuda waliochukua ngao na mikuki, watu 6800 wenye mata ya kupigia vita. Wana wa Simeoni, mafundi wa vita wenye nguvu wajuao kupiga vita, watu 7100. Wana wa Lawi watu 4600, naye Yoyada, mkuu wao wa Haroni, tena pamoja naye watu 3700, naye Sadoki aliyekuwa kijana mwenye nguvu ya kupiga vita, namo mlangoni mwa baba yake wakatoka wakuu 22. Wana wa Benyamini waliokuwa ndugu zake Sauli, watu 3000; kwani mpaka hapo wengi wao walikuwa upande wa mlango wa Sauli na kuulindia. Wana wa Efuraimu, mafundi wa vita wenye nguvu, watu 20800, ni watu waliokuwa wenye macheo katika milango yao. Katika nusu ya shina la Manase wakatoka watu 18000 waliokuwa wameandikwa majina yao, waje, wamfanye Dawidi kuwa mfalme. Wana wa Isakari waliojua kuitambua maana ya siku walijua nayo yaliyowapasa Waisiraeli kufanya, kwa hiyo wakaja wakuu wao 200 nao ndugu zao wote kwa kuagizwa nao. Kwa Zebuluni vikatoka vikosi vya watu waliokuwa tayari kupiga vita kwa kushika vyombo vyote vya vitani, watu 50000 waliozoea kujipanga pasipo kupitana mioyo. Kwa Nafutali wakatoka wakuu 1000, tena pamoja nao watu 37000 wenye ngao na mikuki. Kwa Dani wakatoka waliokuwa tayari kupiga vita, watu 28600. Kwa Aseri watu wakatoka vikosi vizima kwa kuwa tayari kupiga vita, watu 40000. Ng'ambo ya Yordani kwa Rubeni na kwa Gadi na katika nusu ya shina la Manase vikatoka vikosi vyenye vyombo vyote vya vitani, watu 120000. Watu hawa wote wa vita waliojua kujipanga vema vitani wakaja Heburoni, mioyo yao ikiwa mmoja kabisa, wakataka kumfanya Dawidi kuwa mfalme wa Waisiraeli wote; nao Waisiraeli wote waliosalia kwao mioyo yao ilikuwa mmoja tu wakitaka kumfanya Dawidi kuwa mfalme. Wakawa huko pamoja na Dawidi wakila, wakinywa siku tatu, kwani ndugu zao waliwaandalia. Nao waliokaa karibu kwao kuzifikia nchi za Isakari na za Zebuluni na za Nafutali waliwaletea vyakula vikichukuliwa na punda na ngamia na nyumbu na ng'ombe, vilikuwa vilaji vya unga na maandazi ya kuyu na ya zabibu na mvinyo na mafuta na ng'ombe na mbuzi na kondoo wengi, kwa kuwa ilikuwako furaha kwao Waisiraeli. Dawidi akafanya shauri nao wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia na watawalaji wote, kisha Dawidi akauambia mkutano wote wa Waisiraeli: Mkiona kuwa vema, tena vikiwa vimetoka kwake Bwana Mungu wetu, na tutume pande zote po pote kwa ndugu zetu waliosalia katika nchi zote za Isiraeli, hata kwa watambikaji na kwa Walawi katika miji yao, wanamokaa, kuwaambia, wakusanyike kwetu, twende kulichukua Sanduku la Mungu wetu, tulirudishe kwetu, kwani siku za Sauli hatukulitafuta. Watu wote wa huo mkutano wakaitikia, wafanye hivyo, kwa kuwa neno hilo lilikuwa limenyoka machoni pao watu wote. Kwa hiyo Dawidi akawakusanya Waisiraeli wote toka Sihori katika Misri hata kufika Hamati, waje kulichukua Sanduku la Mungu huko Kiriati-Yearimu. Kisha Dawidi na Waisiraeli wote wakapanda kwenda Bala, ndio Kiriati-Yearimu ulio mji wa Yuda, kulichukua huko Sanduku la Mungu Bwana akaaye juu ya Makerubi, kwa maana hili liliitwa kwa Jina lake. Wakalipandisha Sanduku la Mungu katika gari jipya wakilitoa katika nyumba ya Abinadabu, nao Uza na Ayo wakaliendesha hilo gari. Dawidi mwenyewe na Waisiraeli wote wakalitangulia na kucheza mbele ya Mungu kwa nguvu zote na kumwimbia pamoja na kupiga mazeze na mapango na patu na matoazi na matarumbeta. Walipofika pa kupuria pake Kidoni, Uza akapeleka mkono, alishike Sanduku, kwa kuwa ng'ombe walijikwaa. Ndipo, makali ya Bwana yalipomwakia Uza, akampiga, kwa kuwa amelipelekea hilo Sanduku mkono wake, akafa papo hapo mbele ya Mungu. Hapo Dawidi akaingiwa na uchungu, ya kuwa Bwana amempiga Uza pigo kama hilo, wakapaita mahali pale Peresi-Uza (Pigo la Uza) mpaka siku hii ya leo. Siku hiyo Dawidi akashikwa na woga wa kumwogopa Mungu kwamba: Nitawezaje kuliingiza Sanduku la Mungu kwangu? Kwa hiyo Dawidi hakuliingiza Sanduku hilo kwake mjini kwa Dawidi, akashika njia nyingine, akaliweka nyumbani mwa Obedi-Edomu wa Gati. Humo nyumbani mwa Obedi-Edomu Sanduku la Mungu likakaa kwenye mlango wake miezi mitatu, naye Bwana akaubariki mlango wa Obedi-Edomu nayo yote yaliyokuwa yake. Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Dawidi na miti ya miangati na waashi na maseremala, wamjengee Dawidi nyumba. Ndipo, Dawidi alipojua, ya kuwa Bwana amemweka kweli kuwa mfalme wao Waisiraeli, kwani ufalme wake ukaja kutukuka zaidi kwa ajili ya ukoo wake wa Waisiraeli. Kisha Dawidi akachukua wanawake wengine mle Yerusalemu, Dawidi akazaa tena wana wa kiume na wa kike. Haya ndiyo majina ya wana, waliozaliwa Yerusalemu: Samua na Sobabu, Natani na Salomo, Ibuhari na Elisua na Elpeleti, na Noga na Nefegi na Yafia, na Elisama na Beliada na Elifeleti. Wafilisti waliposikia, ya kuwa Dawidi amepakwa mafuta, awe mfalme wao Waisiraeli wote, ndipo, Wafilisti wote walipopanda kumtafuta Dawidi. Dawidi alipovisikia akatoka kukutana nao. Wafilisti wakaja, wakajieneza Bondeni kwa Majitu. Dawidi akamwuliza Mungu kwamba: Nikipanda kupigana na Wafilisti, utawatia mkononi mwangu? Bwana akamwambia: Panda! Nitawatia mkononi mwako. Ndipo, walipopanda Baali-Perasimu; Dawidi alipowapiga huko, akasema yeye Dawidi: Mungu amewaatua adui zangu kwa nguvu ya mkono wangu, kama maji yanavyoatua ukingo. Kwa sababu hii wakapaita mahali pale Baali-Perasimu (Maatuko). Kwa kuwa wale waliiacha huko miungu yao, Dawidi akaagiza iteketezwe kwa moto. Lakini Wafilisti wakapanda tena na kujieneza bondeni kulekuke. Naye Dawidi alipomwuliza Mungu tena, Mungu akamwambia: Usipande kuwafuata, ila uzunguke hapo, walipo, upate kuwajia ukitoka juu, misandarusi iliko. Hapo, utakaposikia vileleni kwa misandarusi shindo kama ya watu wapitao, basi, hapo watokee kupigana nao! Kwani ndipo, Mungu atakapotokea, akutangulie kuyapiga majeshi ya Wafilisti. Dawidi akafanya, kama Mungu alivyomwagiza, wakayapiga majeshi ya Wafilisti toka Gibeoni hata Gezeri. Jina lake Dawidi likaenea katika nchi zote, Bwana akawatia wamizimu wote woga wa kumwogopa. Dawidi akajijengea nyumba mjini mwake, nalo Sanduku la Mungu akalitengenezea mahali na kulipigia hema. Kisha Dawidi akasema: Sanduku la Mungu asilichukue mtu, wasipokuwa Walawi, kwani ndio, Bwana aliowachagua kulichukua Sanduku la Mungu na kumtumikia kale na kale. Dawidi akawakusanya Waisiraeli wote mle Yerusalemu, walipandishe Sanduku la Bwana na kuliweka mahali pake, alipolitengenezea. Dawidi akawakusanya wana wa Haroni na Walawi, kwao wana wa Kehati: mkuu Urieli na ndugu zake, watu 120; kwao wana wa Merari: mkuu Asaya na ndugu zake, watu 220; kwao wana wa Gersomu: mkuu Yoeli na ndugu zake, watu 130; kwao wana wa Elisafani: mkuu Semaya na ndugu zake, watu 200; kwao wana wa Heburoni: mkuu Elieli na ndugu zake, watu 80; kwao wana wa Uzieli: mkuu Aminadabu na ndugu zake, watu 112. Kisha Dawidi akawaita watambikaji Sadoki na Abiatari na Walawi Urieli, Asaya na Yoeli, Semaya na Elieli na Aminadabu, akawaambia: Ninyi m wakuu wa milango ya Walawi, jitakaseni ninyi na ndugu zenu! Kisha mtalipandisha Sanduku la Bwana Mungu wa Isiraeli na kuliweka mahali pake, nilipolitengenezea. Kwa kuwa mara ya kwanza hamkuwako. Bwana Mungu wetu akatupiga pigo, kwa kuwa hatukumtafuta kwa njia itupasayo. Watambikaji na Walawi wakajitakasa, wapate kulipandisha Sanduku la Bwana Mungu wa Isiraeli. Walawi wakalichukua Sanduku la Mungu kwa kuweka mipiko mabegani pao, kama Mose alivyoagiza kwa kuambiwa na Bwana. Kisha Dawidi akawaambia wakuu wa Walawi, wawapange ndugu zao waimbaji, wakivishika vyombo vyao vya kuimbia: mapango na mazeze na matoazi, wapige shangwe na kuzipaza sauti kwa furaha. Ndipo, Walawi walipowapanga: Hemani, mwana wa Yoeli, na kwa ndugu zake: Asafu, mwana wa Berekia, na kwa wana wa Merari walio ndugu zao: Etani, mwana wa Kusaya. Pamoja nao wakawapanga ndugu zao wa uzao wa pili: Zakaria, Beni na Yazieli, na Semiramoti na Yehieli na Uni, Eliabu na Benaya na Masea na Matitia na Elifelehu na Mikinea na Obedi-Edomu na Yieli waliokuwa walinda malango. nao waimbaji Hemani, Asafu na Etani walioshika matoazi ya shaba, wayavumishe, na Zakaria na Azieli na Semiramoti na Yehieli na Uni na Eliabu na Masea na Benaya walioshika mapango, waimbe sauti za juu; na Matitia na Elifelehu na Mikinea na Obedi-Edomu na Yieli na Azazia walioshika mazeze, waimbe sauti za chini na kuwaongoza wengine. Kenania, mkuu wa Walawi, aliyewaimbisha akawasimamia, walipoimba, kwani aliijua kazi hiyo. Naye Berekia pamoja na Elkana wakayangoja malango penye Sanduku la Agano. Nao watambikaji Sebania na Yosafati na Netaneli na Amasai na Zakaria na Benaya na Eliezeri wakalitangulia Sanduku la Mungu na kupiga matarumbeta, nao Obedi-Edomu na Yehia wakayalinda malango penye sanduku hilo. Ndivyo, Dawidi na wazee wa Waisiraeli na wakuu wa maelfu walivyokwenda kulipandisha Sanduku la Agano la Bwana wakilitoa nyumbani mwa Obedi-Edomu kwa furaha. Kwa sababu Mungu aliwasaidia Walawi waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana, wakamtolea ng'ombe saba kuwa za tambiko pamoja na madume saba ya kondoo. Dawidi alikuwa amevaa kanzu ya bafta, hata Walawi wote waliolichukua hilo Sanduku na waimbaji na Kenania, mkuu wao waimbaji aliyewaimbisha, naye Dawidi alikuwa amevaa kisibau cheupe cha ukonge. Nao Waisiraeli wote wakalipandisha Sanduku la Agano la Bwana kwa kushangilia na kwa kupiga mabaragumu na matarumbeta na matoazi pamoja na kuyavumisha nayo mapango na mazeze. Ikawa, Sanduku la Agano la Bwana lilipoingia mjini kwa Dawidi, Mikali, binti Sauli, alichungulia dirishani, naye alipomwona mfalme Dawidi, jinsi alivyorukaruka na kuchezacheza, ndipo, alipombeza moyoni mwake. Walipokwisha kuliingiza Sanduku la Mungu wakaliweka katikati ya lile hema, Dawidi alilolipigia, wakamtolea Mungu ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kumshukuru. Dawidi alipokwisha kuzitoa hizo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani akawabariki watu katika Jina la Bwana. Kisha akawagawia watu wote wa Isiraeli, waume kwa wake, kila mtu mkate wa sikukuu na kipande cha nyama na andazi la zabibu. Akaweka Walawi wengine, watumike hapo penye Sanduku la Bwana na kuwakumbusha watu, Bwana Mungu wa Isiraeli aliyoyafanya, wamshukuru na kumtukuza, ndio mkuu Asafu na Zakaria aliyekuwa mkuu wa pili, tena Yieli na Semiramoti na Yehieli na Matitia na Eliabu na Benaya na Obedi-Edomu na Yieli, wavishike vyombo vya kuimbia, mapango na mazeze, naye Asafu ayapige matoazi. Nao watambikaji Benaya na Yahazieli wapige matarumbeta siku zote mbele ya Sanduku la Agano la Mungu. Siku hiyo ndipo, Dawidi alipoagiza kwanza kumshukuru Bwana kwa msaada wa Asafu na wa ndugu zake: Mshukuruni Bwana, nalo Jina lake litambikieni! Yajulisheni makabila ya watu matendo yake! Mpigieni shangwe za kumwimbia! Mataajabu yake yote yatungieni tenzi! Lishangilieni Jina lake lililo takatifu! Mioyo yao wamtafutao Bwana na ifurahi! Mchungulieni Bwana nazo nguvu zake! Utafuteni uso wake siku zote! Yakumbukeni mataajabu yake, aliyoyafanya. nayo maamuzi yake yashangazayo yakisemwa na kinywa chake! Ninyi mlio uzao wake Isiraeli aliyemtumikia, nanyi wana wa Yakobo, yeye aliyemchagua! Yeye Bwana ni Mungu wetu, nchi zote anaziamua. Likumbukeni Agano lake kale na kale! Aliowaagiza kulishika Neno lake ni vizazi elfu. Agano ni lile, alilomwekea Aburahamu, nacho kiapo ni kile, alichomwapia Isaka. Mbele yake Yakobo naye akalisimamisha kuwa maongozi, Agano la kale na kale liwe kwake Isiraeli kwamba: Wewe ndiwe, nitakayekupa nchi ya Kanaani. iwe fungu lenu, nililowapimia. Vilikuwa hapo, walipokuwa kikundi cha watu wanaohesabika, maana kule walikuwa wachache tu, tena wageni. Wakawaendea watu wa huko, taifa kwa taifa, walipotoka kwa mfalme mmoja, wakawajia wenziwe. Lakini hakuna mtu, aliyempa ruhusa kuwakorofisha, hata wafalme akawapatiliza kwa ajili yao kwamba: Niliowapaka mafuta msiwaguse tu, wala wafumbuaji wangu msiwafanyizie mabaya! Mwimbieni Bwana, nchi zote! Utangazeni wokovu wake siku kwa siku! Wasimulieni wamizimu utukufu wake, nako kwenye makabila yote ya watu mataajabu yake! Kwani mkuu ni Bwana, apaswa na kutukuzwa sana, naye anaogopesha kuliko miungu yote. Kwani miungu yote ya makabila ya watu ni ya bure tu, lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu. Ukuu na urembo uko mbele yake, uwezo na uchangamko upo hapo, alipo. Ninyi mlio wa ukoo wa watu, mpeni Bwana yaliyo yake! Kwa kuwa ni mtukufu na mnguvu, mpeni Bwana yaliyo yake! Kwa kuwa Jina lake ni tukufu, mpeni Bwana yaliyo yake! Chukueni vipaji vya tambiko, mje kumtokea! Mtambikieni Bwana na kuvaa mapambo yapasayo Patakatifu! Mkimtokea, mastuko na yawaguie, ninyi wa nchi zote! Yeye ndiye aliyeishikiza nchi, isije kuyumbayumba! Kwa hiyo mbingu na zifurahi, nchi nayo na ipige shangwe! Nako kwa wamizimu na waseme: Bwana ni mfalme! Hata bahari nayo yote yajaayo ndani yake na yavume! Mashamba nayo yote yaliyomo na yapige vigelegele! Itakuwa, nayo miti yote ya mwituni imshangilie Bwana, kwani ndiye atakayekuja kuihukumu nchi. Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema! Ya kuwa upole wake ni wa kale na kale! Semeni: Tuokoe, Mungu uliye wokovu wetu! Tukusanye na kutuponya kwenye wamizimu, tupate kulishukuru Jina lako takatifu, tuzidishe kukusifu na kukushangilia! Na atukuzwe Bwana Mungu wa Isiraeli, tangu kale hata kale! Watu wote wakaitika: Amin! Haleluya! Huko kwenye Sanduku la Agano la Bwana Dawidi akamwacha Asafu na ndugu zake, watumikie mbele ya hilo Sanduku pasipo kukoma wakifanya kazi ipasayo kila siku moja. Tena akamweka Obedi-Edomu pamoja na ndugu zake 68, huyu Obedi-Edomu, mwana wa Yedutuni, na Hosa wawe walinda malango. Naye mtambikaji Sadoki na watambikaji ndugu zake akawaacha mbele ya Kao la Bwana kule kilimani kwenye Gibeoni, wamtolee Bwana mezani pa kutambikia pasipo kukoma asubuhi na jioni ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na kuyafanya yote yaliyoandikwa katika Maonyo ya Bwana, aliyoyaagiza, Waisiraeli wayafanye. Pamoja nao walikuwako Hemani na Yedutuni nao wengine wote waliochaguliwa na kuandikwa majina, waimbe: Mshukuruni Bwana, ya kuwa upole wake ni wakale na kale! Akina Hemani na Yedutuni waliokuwa nao, wakapewa matarumbeta na matoazi ya kuwapa wenye kuyapiga na vyombo vyote vya kuimbia nyimbo za Mungu. Nao wana wa Yedutuni wakalinda langoni. Kisha watu wote wakaenda kila mtu nyumbani kwake, naye Dawidi akazunguka kuubariki mlango wake. Ikawa, Dawidi alipokaa nyumbani mwake, Dawidi akamwambia mfumbuaji Natani: Tazama, mimi ninakaa katika nyumba iliyojengwa kwa miangati, lakini Sanduku la Agano la Bwana linakaa chini ya mapazia tu. Natani akamwambia Dawidi: Yote yaliyomo moyoni mwako yafanye! Kwani Mungu yuko pamoja na wewe. Lakini usiku uleule neno la Mungu likamjia Natani kwamba: Nenda, umwambie mtumishi wangu Dawidi: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa. Kwani sikukaa nyumbani tangu siku ile, nilipowaleta Waisiraeli huku milimani, mpaka siku hii ya leo, ila nilikuwa hemani huku, tena hamani huko, Kao langu likawa huku na huko. Je? Hapo pote, nilipokwenda pamoja na Waisiraeli wote, nilimwambia hata mmoja wao waamuzi wa Waisiraeli, niliowaagiza kuwachunga walio ukoo wangu, na kumwuliza neno la kwamba: Mbona hamnijengei nyumba ya miangati? kwa hiyo umwambie sasa mtumishi wangu Dawidi: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mimi nilikuchukua malishoni, ulipowafuata kondoo, uwe nwenye kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli. Nikawa pamoja na wewe po pote, ulipokwenda, nikawaangamiza adui zako wote mbele yako; nitakupatia jina lililo sawa na majina ya wakubwa walioko huku nchini. Nao walio ukoo wangu wa Waisiraeli nitawapatia mahali, nitakapowapanda, wapate kukaa hapo pasipo kuhangaika tena, wala watu waovu wasiwakorofishe tena kama huko kwanza tangu siku zile nilipowaagiza waamuzi, wawatawale walio ukoo wangu wa Waisiraeli; nitawanyenyekeza adui zako wote, tena ninakuambia sasa: Bwana atakujengea nyumba. Itakuwa hapo, siku zako zitakapotimia, uende kulala pamoja na baba zako; ndipo, nitakapoinua nyuma yako mzao wako atakayetoka kwa wanao, niusimike ufalme wake. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakisimamisha kiti chake cha kifalme, kipate kuwapo kale na kale. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu, nao upole wangu sitauondoa kwake, kama nilivyouondoa kwao waliokuwa mbele yako. Nitamsimamisha, awe nyumbani mwangu namo katika ufalme wangu kale na kale, nacho kiti chake cha kifalme kitakuwa kimesimamishwa kale na kale. Natani akamwambia Dawidi haya maneno yote sawasawa, kama alivyoyaona yote alipoyachunguza. Kisha mfalme Dawidi akaingia pake Bwana, akakaa hapo akisema: Bwana Mungu, mimi ni nani? Nao mlango wangu ni nini ukinileta, nifike hapa? Lakini haya yakawa madogo machoni pako, Mungu, kwa hiyo umeyasema yatakayoujia mlango wa mtumishi wako katika siku zilizo mbali bado, ukanitazama kimtu na kunikweza, Bwana Mungu. Dawidi akuambie nini tena kwa hivyo, unavyomheshimu mtumishi wako? Wewe unamjua mtumishi wako. Bwana, kwa ajili ya mtumishi wako na kwa mapenzi ya moyo wako umeyafanya haya makubwa yote, uyajulishe haya matendo makubwa yote. Bwana, hakuna anayefanana na wewe, hakuna Mungu, asipokuwa wewe, kwa hayo yote, tuliyoyasikia kwa masikio yetu. Tena liko taifa moja tu huku nchini linalofanana na ukoo wako wa Waisiraeli? Hao ndio, Mungu aliokwenda kuwakomboa, wawe ukoo wake. Hapo ulijipatia Jina kwa matendo makubwa yaliyoogopesha, ulipowafukuza wamizimu mbele yao walio ukoo wako, uliowakomboa na kuwatoa Misri. Ukaupa ukoo wako wa Waisiraeli kuwa ukoo wako kale na kale, wewe Bwana ukawa Mungu wao. Sasa Bwana, neno hili, ulilolisema la mtumishi wako na la mlango wake, liwe limeshupaa kale na kale, ukifanya, kama ulivyosema. Ndivyo, Jina lako litakavyokuwa limeshupaa kwa kuwa kubwa kale na kale kwamba: Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, ni Mungu wa Isiraeli kweli, tena ndivyo, mlango wa mtumishi wako Dawidi utakavyokuwa wenye nguvu mbele yako. Kwani wewe, Mungu wangu, umelifunua sikio la mtumishi wako, asikie, ya kuwa utamjengea nyumba, kwa hiyo mtumishi wako ameiona njia hii ya kukutolea maombo haya. Sasa Bwana, wewe ndiwe Mungu; hayo mema, uliyomwambia mtumishi wako, na yapate kuwa. Sasa na ikupendeze kuubariki mlango wa mtumishi wako, uwepo kale na kale usoni pako! Kwani unayoyabariki wewe, Bwana, huwa yamebarikiwa kale na kale. Hayo yalipokwisha, Dawidi akawapiga Wafilisti, akawashinda, akauchukua Gati na vijiji vyake mikononi mwa Wafilisti. Akawapiga nao Wamoabu, hao Wamoabu wakawa watumishi wa Dawidi, wakamletea mahongo. Kisha Dawidi akampiga Hadarezeri, mfalme wa Soba ulioko upande wa Hamati, alipokwenda kuusimika tena ufalme wake huko kwenye jito la Furati. Dawidi akateka kwake magari 1000, na wapanda farasi 7000 na askari waliokwenda kwa miguu 20000, nao farasi wote wa kuvuta magari Dawidi akawakata mishipa ya miguu, akajisazia farasi wa magari mia tu. Washami wa Damasko walipokuja kumsaidia Hadarezeri, mfalme wa Soba, Dawidi akapiga kwao Washami watu 22000. Dawidi akaweka askari kwao Washami wa Damasko, hao Washami wakawa watumishi wa Dawidi, wakamletea mahongo. Ndivyo, Bwana alivyompa Dawidi kushinda pote, alipokwenda. Dawidi akazichukua ngao za dhahabu, watumishi wa Hadarezeri walizokuwa nazo, akazipeleka Yerusalemu. Namo mle Tibehati na Kuni iliyokuwa miji ya Hadarezeri Dawidi akachukua shaba nyekundu nyingi mno; ndizo, Salomo alizozitumia za kutengeneza ile bahari ya shaba nazo zile nguzo navyo vyombo vya shaba. Tou, mfalme wa Hamati, aliposikia, ya kuwa Dawidi amevipiga vikosi vyote vya Hadarezeri, mfalme wa Soba, akamtuma mwanawe Hadoramu kwake mfalme Dawidi kumpongeza na kumbariki, kwa kuwa amepigana na Hadarezeri na kumshinda, kwani Tou na Hadarezeri walikuwa wakipigana vita; akampelekea vyombo vyo vyote vya dhahabu na vya fedha na vya shaba. Hivi navyo mfalme Dawidi akavitakasa kuwa mali za Bwana kama fedha na dhahabu, alizoziteka kwa mataifa yote, kwa Waedomu na kwa Wamoabu na kwa wana wa Amoni na kwa Wafilisti na kwa Waamaleki. Naye Abisai, mwana wa Seruya, akawapiga Waedomu Bondeni kwa Chumvi, watu 18000. Kisha Dawidi akaweka askari kwa Waedomu, nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Dawidi. Ndivyo, Bwana alivyompa Dawidi kushinda po pote, alipokwenda. Dawidi akawa mfalme wa Waisiraeli wote, akawatengenezea watu wake wote mashauri yaliyokuwa sawa, maana yaliongoka. Naye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa vikosi, naye Yosafati, mwana wa Ahiludi, alikuwa mwandishi wa mambo yaliyopaswa kukumbukwa. Naye Sadoki, mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki, mwana wa Abiatari, walikuwa watambikaji, naye Sausa alikuwa mwandishi. Naye Benaya, mwana wa Yoyada, alikuwa mkuu wa Wakreti na wa Wapuleti, nao wana wa Dawidi walikuwa wa kwanza mkononi kwa mfalme. Hayo yalipokwisha, akafa Nahasi, mfalme wa wana wa Amoni, naye mwanawe akawa mfalme mahali pake. Dawidi akasema: Nitamfanyizia Hanuni, mwana wa Nahasi, mambo ya upole, kwani baba yake alinifanyizia nami mambo ya upole. Kwa hiyo Dawidi akatuma wajumbe, wamtulize moyo kwa ajili ya baba yake. Lakini watumishi wa Dawidi walipofika katika nchi ya wana wa Amoni kwake Hanuni, wamtulize moyo, wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia Hanuni: Je? Dawidi anataka kweli kumheshimu baba yako machoni pako akituma kwako wajumbe wa kukutuliza moyo? Watumishi wake hawakuja kwako kuichunguza nchi na kuifudikiza na kuipeleleza? Ndipo, Hanuni alipowakamata watumishi wa Dawidi, akawanyoa nywele, akawakatia mavazi yao nusu kuyafikisha matako yao, kisha wakawapa ruhusa kwenda zao, wakaenda zao. Watu walipompasha Dawidi habari za hao watu, akatuma wengine kuwaendea njiani, kwa kuwa watu hao walikuwa wametwezwa sana; mfalme akawaambia: Kaeni Yeriko, mpaka ndevu zenu zikue tena, kisha rudini! Wana wa Amoni walipoona, ya kuwa wamejichukizisha kwake Dawidi, ndipo, Hanuni na wana wa Amoni walipotuma vipande elfu vya fedha, ndio shilingi milioni moja na 200000, wakodishe magari na wapanda farasi kwa Washami wa Mesopotamia na kwa Washami wa Maka nako Soba. Wakakodisha magari 32000 pamoja na mfalme wa Maka na watu wake, wakaja, wakapiga makambi mbele ya Medeba, nao wana wa Amoni wakakusanyika wakitoka mijini kwao, wakaja vitani. Dawidi alipoyasikia, akamtuma Yoabu na vikosi vyote vya mafundi wa vita. Wana wa Amoni wakatoka, wakajipanga penye lango la mji, wapige vita, nao wafalme waliokuja wakawa peke yao shambani. Yoabu alipoona, ya kuwa wamejipanga kupiga vita usoni na mgongoni kwake, akachagua wengine katika wateule wote wa Waisiraeli, akawapanga, wapigane na Washami. Nao watu waliosalia akawatia mkononi mwa ndugu yake Abisai, wakawapanga, wapigane na wana wa Amoni. akasema: Kama Washami wanapata nguvu za kunishinda, sharti uje kunisaidia. Tena kama wana wa Amoni wanapata nguvu za kukushinda, sharti nije, nikusaidie. Jipe moyo, tushikizane mioyo, tuwapiganie watu wa kwetu na miji ya Mungu wetu! Ndipo, Bwana atakapoyafanya, aliyoyaona kuwa mema. Kisha Yoabu na watu wake, aliokuwa nao, wakawasogelea Washami kupigana nao, lakini wao wakawakimbia. Wana wa Amoni walipoona, ya kuwa Washami wamekimbia, ndipo, nao walipomkimbia ndugu yake Abisai, wakaingia mjini mwao, lakini Yoabu akaja Yerusalemu. Washami walipoona, ya kuwa wameshindwa nao Waisiraeli, wakatuma wajumbe, wakawaita Washami walioko ng'ambo ya huko ya jito hilo, waje vitani, naye Sofaki, mkuu wa vikosi vya Hadarezeri, akawaongoza. Dawidi alipopashwa habari hizo, akawakusanya Waisiraeli wote, akauvuka Yordani, akawajia, akajipanga mbele yao. Dawidi alipokwisha kujipanga kupiga vita na Washami, wakapigana naye. Kisha Washami wakawakimbia Waisiraeli, Dawidi akaua kwao Washamu watu 7000 waliopanda magari na watu 40000 waliokwenda kwa miguu, hata Sofaki, mkuu wa vikosi, akamwua. Watumishi wa Hadarezeri walipoona, ya kuwa wameshindwa na Waisiraeli, wakafanya mapatano na Dawidi, wakamtumikia; kisha Washami hawakutaka kuwasaidia wana wa Amoni tena. Ikawa, mwaka ulipopita, siku hizo, wafalme wanapozoea kwenda vitani, Yoabu akavipeleka vikosi vya askari, akaiangamiza nchi ya wana wa Amoni, akaja, akausonga mji wa Raba kwa kuuzinga, lakini Dawidi alikuwa anakaa Yerusalemu. Yoabu akaupiga Raba, akaubomoa. Ndipo, Dawidi alipoliondoa taji la mfalme wao kichwani pake, akaliona uzito wake kuwa frasila tatu za dhahabu, nalo lilikuwa limepambwa kwa vito vyenye kima; hilo Dawidi akavikwa kichwani. Namo mjini akatoa mateka mengi sana. Nao watu waliokuwamo akawatoa, akawakatakata kwa misumeno na kwa magari ya chuma ya kupuria na kwa mashoka. Hivyo Dawidi akaifanyizia miji yote ya wana wa Amoni. Kisha Dawidi akarudi Yerusalemu pamoja na watu wote. Ikawa, hayo yalipokwisha, yakatokea mapigano na wafilisti kule Gezeri; huko ndiko, Sibekai wa Husa alikompiga Sipai aliyekuwa mmoja wao yale Majitu marefu; ndivyo, walivyoshindwa. Kisha yakawa tena mapigano na Wafilisti; ndipo, Elihanani, mwana wa Yairi, alipompiga Lahami, nduguye Goliati wa Gati aliyekuwa na mkuki wenye uti kama majiti ya wafuma nguo. Kisha yakawa mapigano tena kule Gati; huko kulikuwa na mtu mrefu sana mwenye vidole sita sita mikononi na miguuni, vyote pamoja ni 24, naye alikuwa mmoja wao yale Majitu marefu. Alipowatukana Waisiraeli, Yonatani, mwana wa Simea, kaka yake Dawidi, akampiga. Hao walikuwa wamezaliwa katika mlango wa Majitu marefu huko Gati, wakauawa kwa mikono ya Dawidi na kwa mikono ya watumishi wake. Satani akawainukia Waisiraeli akimponza Dawidi, awahesabu Waisiraeli. Dawidi akamwambia Yoabu na wakuu wa watu: Nendeni, mwahesabu Waisiraeli toka Beri-Seba hata Dani! Kisha nileteeni habari, nipate kuzijua hesabu zao. Yoabu akamjibu: Bwana na aendelee kuwaongeza watu wake vivyo hivyo mara mia! Bwana wangu mfalme, kumbe wao wote sio watumishi wa bwana wangu? Hayo bwana wangu anayatakia nini? Kuwakosesha Waisiraeli hivyo ni kwa nini? Lakini neno la mfalme likapata nguvu, asimsikie Yoabu; ndipo, Yoabu alipotoka, akaenda po pote kwao Waisiraeli, kisha akaja Yerusalemu. Hapo Yoabu akampasha Dawidi habari za jumla ya watu waliohesabiwa, wakawa Waisiraeli wote watu milioni moja na 100000 wenye kushika panga, nao Wayuda walikuwa watu 470000 wenye kushika panga. Walawi na Wabenyamini hakuwahesabu, kwani hilo neno la mfalme lilikuwa limemchukiza Yoabu. Neno hili likawa baya machoni pake Mungu, kwa hiyo akawapiga Waisiraeli. Ndipo, Dawidi alipomwambia Mungu: Nimekosa sana kwa kulifanya neno hilo; sasa umwondolee mtumishi wako hizo manza, alizozikora! Kwani nimefanya kisichopasa kabisa. Lakini Bwana akamwambia Gadi aliyekuwa mchunguzaji wake Dawidi kwamba: Nenda kumwambia Dawidi kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mimi ninakuwekea mambo matatu, ndimo uchague moja lao, nikufanyizie. Gadi akaja kwa Dawidi, akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Jipatie ulitakalo! Unataka miaka mitatu ya njaa? au unataka kukimbizwa miezi mitatu machoni pao wakusongao, panga za adui zako zikikupata? au unataka, upanga wa Bwana na ugonjwa mbaya uuao upite katika nchi hii, malaika wa Bwana akifanya maovu katika mipaka yote ya Waisiraeli? Sasa tafuta, uone nitakayomjibu aliyenituma! Dawidi akamwambia Gadi: Nimesongeka sana, lakini na nijitupe mkononi mwake Bwana, kwani huruma zake ni nyingi mno nisijitupe mikononi mwa watu. Ndipo, Bwana alipowauguza Waisiraeli ugonjwa mbaya uuao, wakafa kwa Waisiraeli watu 70000. Mungu akamtuma malaika wake namo Yerusalemu, afanye humo namo maovu yake; lakini Bwana alipoyaona hayo maovu, aliyoyafanya, akageuza moyo kwa ajili ya huo ubaya, akamwambia yule malaika aliyeangamiza: Sasa inatosha, ulegeze mkono wako! Naye yule malaika wa Bwana alikuwa akisimama penye kupuria ngano pa Myebusi Ornani. Dawidi alipoyainua macho yake, akamwona malaika wa Bwana, akisimama kati ya nchi na ya mbingu, nao upanga uliochomolewa ulikuwa mkononi mwake kuuelekea Yerusalemu; ndipo, Dawidi na wazee waliokuwa wamevaa magunia walipoanguka kifudifudi, Dawidi akamwambia Mungu: Kumbe si mimi niliyeagiza kuwahesabu watu? Mimi ndiye niliyekosa na kufanya mabaya sana. Lakini hawa kondoo wamefanya nini? Bwana Mungu wangu, mkono wako na unipige mimi na mlango wa baba yangu! Lakini hawa walio ukoo wako usiwaue! Ndipo, malaika wa Bwana alipomwambia Gadi, amwambie Dawidi, Dawidi apande kutengeneza pa kumtambikia Bwana papo hapo penye kupuria ngano pa Myebusi Ornani. Kwa hilo neno, Gadi alilolisema katika Jina la Bwana, Dawidi akapanda. Ornani alipogeuka akamwona malaika; nao wanawe wanne waliokuwa naye walikuwa wamejificha, naye Ornani mwenyewe alikuwa akipura ngano. Dawidi alipokuja kwake Ornani, huyu Ornani alikuwa akitazama; alipomwona Dawidi, akatoka hapo pa kupuria ngano, akamwangukia Dawidi usoni hapo chini. Dawidi akamwambia Ornani: Nipe mahali hapa pa kupuria ngano, nipajenge pa kumtambikia Bwana! Nitakulipa fedha zote zipapasazo, nipe tu mahali hapa, huku kuuawa kwa watu kukomeshwe! Ornani akamwambia Dawidi: Jichukulie tu! Bwana wangu mfalme na afanye, anayoyaona kuwa mema. Tazama, nakupa hawa ng'ombe kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, nayo haya magari nakupa kuwa kuni, nazo hizi ngano zote nakupa kuwa vilaji vya tambiko. Mfalme Dawidi akamwambia ornani: Sivyo, kwani nitanunua kabisa na kulipa fedha zote zipapasazo, kwani sitazichukua mali zako za kumtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, nisizozilipa. Dawidi akampa Ornani kwa kupanunua mahali pale vipande vya dhahabu 600 vilivyokuwa kama shilingi 45000. Kisha Dawidi akamjengea Bwana hapo mahali pa kumtambikia, akamtolea ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na vipaji vya tambiko vya kumshukuru, akamwita Bwana na kumwomba, naye akamwitikia akitoa moto mbinguni, upaangukie hapo pa kumtambikia kwa kumtolea ng'ombe za kuteketezwa nzima. Ndipo, Bwana aliposema na yule malaika, naye akaurudisha upanga wake alani mwake. Kwa kuwa Dawidi aliona wakati huo, ya kuwa Bwana amemwitikia hapo pa kupuria ngano pa Myebusi Ornani, huja kutambikia hapo. Nalo kao la Bwana, Mose alilolitengeneza nyikani, pamoja na meza ya kumteketezea Bwana ng'ombe za tambiko siku zile lilikuwa kilimani kwa Gibeoni. Lakini Dawidi hakuweza kwenda huko kumtafuta Mungu, kwa kuwa alikuwa ametishwa na upanga wa yule malaika wa Bwana. Dawidi akasema: Hapa ndipo mahali pa nyumba ya Bwana Mungu, ndipo napo, Waisiraeli watakapoteketezea ng'ombe za tambiko. Dawidi akaagiza, wageni walioko katika nchi ya Waisiraeli wakusanyike, akaweka mafundi wa kuchonga, wachonge mawe ya jengo ya kuijenga nyumba ya Mungu. Tena Dawidi akaweka vyuma vingi vya misumari ya kutilia milango malangoni na vya mapapi na shaba nyingi zisizopimika. Tena miti mingi ya miangati isiyohesabika, kwani Wasidoni na Watiro wakamletea Dawidi miti mingi ya miangati. Maana Dawidi aliwaza moyoni kwamba: Mwanangu Salomo ujana wake ungali mchanga bado, nayo nyumba, Bwana atakayojengewa sharti iwe kubwa zaidi, ipate jina lenye utukufu katika nchi hizi zote, kwa hiyo nitamwandalia yaipasayo. Kwa sababu hii Dawidi akaandaa mengi, kabla hajafa. Kisha akamwita mwanawe Salomo, akamwagiza kumjengea Bwana Mungu wa Isiraeli nyumba. Hapo Dawidi akamwambia Salomo: Mwanangu, mimi nalitaka kwa moyo kulijengea Jina la Bwana Mungu wangu nyumba. Lakini neno la Bwana likanijia la kwamba: Umemwaga damu nyingi kwa kupiga vita vikubwa, hutalijengea Jina langu nyumba, kwa kuwa umemwaga damu nyingi chini mbele yangu. Tazama, kwako atazaliwa mwana, yeye atakuwa mtu wa kutulia, nami nitamtulizia adui zake wote pande zote, kwani jina lake ataitwa Salomo (Mtulivu), nami nitampatia utengemano na utulivu kwao Waisiraeli katika siku zake. Yeye atalijengea Jina langu nyumba, naye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake, nami nitakishupaza kiti cha ufalme wake, kisimame kwao Waisiraeli kale na kale. Sasa mwanangu, Bwana awe na wewe, ufanikiwe ukimjengea Bwana Mungu wako nyumba, kama alivyosema kwa ajili yako wewe. Tena Bwana na akupe akili na utambuzi, atakapokuagiza kuwa mkuu wao Waisiraeli, uyaangalie Maonyo ya Bwana Mungu wako! Ndivyo, utakavyofanikiwa ukiyaangalia maongozi na maamuzi, Bwana aliyamwagiza Mose ya kutumia kwao Waisiraeli. Jipe moyo, upate nguvu, usiogope, wala usiingiwe na vituko! Tazama, ingawa nimekuwa mwenye masumbuko, nyumba ya Bwana nimeiwekea vipande vya dhahabu elfu mia, ndio shilingi kama milioni 22000 na vipande vya fedha milioni moja, ndio shilingi kama milioni 12000, tena shaba na vyuma visivyopimika kwa kuwa vingi; hata miti na mawe nimeweka, lakini haya utayaongeza. Hata mafundi unao wengi, wachonga mawe na waashi na maseremala, tena kwa kila kazi wako wanaoijua vema. Dhahabu na fedha na shaba na vyuma havihesabiki; haya! Inuka, kazifanye kazi hizo! Naye Bwana na awe na wewe! Kisha Dawidi akawaagiza wakuu wote wa Waisiraeli kumsaidia mwanawe Salomo, akisema: Je? Bwana Mungu wenu hakuwa nanyi akiwapatia kutulia pande zote? Kwani wote waliokaa katika nchi hii amewatia mkononi mwangu, nchi hii yote ikashurutishwa kumtii Bwana nao walio ukoo wake. Sasa jipeni mioyo na kuzikaza roho zenu, mmtafute Bwana Mungu wenu! Inukeni, pajengeni Patakatifu pa Bwana Mungu, mlipeleke Sanduku la Agano la Bwana na vyombo vitakatifu vya Mungu katika nyumba hiyo itakayojengewa Jina la Bwana! Dawidi alipokuwa mzee mwenye kushiba siku za kuwapo, akampa mwanawe Salomo ufalme wa Waisiraeli, akawakusanya wakuu wote wa Waisiraeli na watambikaji na Walawi. Hapo Walawi waliomaliza miaka thelathini na zaidi walipohesabiwa, ikawa hesabu yao ya vichwa vya waume 38000. Katika hawa wakapewa watu 24000 kuziangalia kazi za nyumba ya Bwana, watu 6000 kuwa wenye amri na waamuzi, watu 4000 kuwa walinda malango, tena watu 4000 kumtukuza Bwana kwa vyombo, Dawidi alivyovitengeneza vya kumtukuza Bwana. Kisha Dawidi akawagawanya kuwa mafungu yao wana wa Lawi, ndio Gersoni, Kehati na Merari. Wagersoni ni Ladani na Simei. Wana wa Ladani walikuwa watatu: mkubwa Yehieli, tena Zetamu na Yoeli. Wana wa simei walikuwa watatu: Selomiti na Hazieli na Harani. Hawa ndio wakubwa wa mlango wa Ladani. Wana wa Simei walikuwa: Yahati na Zina na Yeusi na Beria, hawa wanne walikuwa wana wa Simei. Naye Yahati alikuwa mkubwa, naye Ziza wa pili; lakini Yeusi na Beria hawakuwa na wana wengi, kwa hiyo walihesabiwa kuwa mlango mmoja. Wana wa Kehati walikuwa wanne: Amuramu, Isihari, Heburoni na Uzieli. Wana wa Amuramu walikuwa Haroni na Mose. Haroni akatengwa na kutakaswa, apatumikie Patakatifu Penyewe, yeye na wanawe kale na kale, wamvukizie Bwana kwa utumishi wao, tena wawabariki watu katika Jina lake kale na kale. Naye Mose akawa mtu wa Mungu, wanawe wakatajwa majina yao penye shina la Lawi. Wana wa Mose walikuwa Gersomu na Eliezeri. Wana wa Gersomu mkubwa wao alikuwa Sebueli. Wana wa Eliezeri mkubwa wao alikuwa Rehabia; yeye Eliezeri hakuwa na wana wengine, lakini wana wa Rehabia walikuwa wengi zaidi. Wana wa Isahari mkubwa wao alikuwa Selomiti. Wana wa Heburoni mkubwa wao alikuwa Yeria, wa pili Amaria, wa tatu Yahazieli na wa nne Yekamamu. Wana wa Uzieli mkubwa wao alikuwa Mika, wa pili Isia. Wana wa Merari walikuwa Mahali na Musi, nao wana wa Mahali walikuwa Elazari na Kisi. Elazari akafa pasipo kupata wana wa kiume, alipata wa kike tu, nao wana wa Kisi wakawaoa hao ndugu zao. Wana wa Musi walikuwa watatu: Mahali na Ederi na Yeremoti. Hawa ndio wana wa Lawi kwa milango yao nao wakuu wa milango, kama walivyoandikwa kichwa kwa kichwa kwa hesabu ya majina yao, ndio waliofanyia nyumba ya Bwana kazi za utumishi, waliomaliza miaka ishirini na zaidi; kwani Dawidi alisema: Kwa kuwa Bwana Mungu wa Isiraeli ameupatia ukoo wake utulivu, tena kwa kuwa atakaa Yerusalemu kale na kale, sasa Walawi hawana tena kazi za kulichukua hilo Kao na vyombo vyake vyote vya kulitumikia. Kwani kwa maagizo ya Dawidi ya mwisho wana wa Lawi walihesabiwa wao waliomaliza miaka ishirini na zaidi. Tangu hapo kazi zao zikawa kuwasaidia wana wa Haroni, wakiitumikia nyumba ya Bwana, waziangalie nyua na vyumba, wayasafishe matakatifu yote; hizi zikawa kazi zao za utumishi wa nyumba ya Mungu. Tena iliwapasa kuiandaa mikate, aliyowekewa Bwana, na unga uliopepetwa vema wa vilaji vya tambiko na wa maandazi membamba yasiyochachwa na wa vikate vilivyochomwa katika bati la chuma na wa vitumbua na kuviangalia vibaba na vipimo vyote pia. Tena iliwapasa kusimama siku kwa siku kulipokucha, wakimshukuru Bwana na kumtukuza, na vilevile kulipokuchwa. Tena iliwapasa kumtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima za siku za mapumziko na za miandamo ya mwezi na za sikukuu kwa hesabu zao zilizowekwa za kumtolea Bwana pasipo kukoma. Hivyo walishika zamu ya Hema la Mkutano na zamu ya Patakatifu na zamu ya kuwasaidia ndugu zao wana wa Haroni wakitumikia nyumbani mwa Bwana. Mafungu yao wana wa Haroni ni haya: wana wa Haroni walikuwa Nadabu na Abihu, Elazari na Itamari. Nadabu na Abihu wakafa, baba yao akingalo yupo, nao hawakuwa na wana; kwa hiyo Elazari na Itamari wakaupata utambikaji. Dawidi akapatana na Sadoki aliyekuwa wa wana wa Elazari na Ahimeleki aliyekuwa wa wana wa Itamari, akawagawanya, kama walivyokuwa na ukuu katika utumishi wao. Hapo ikatokea, ya kuwa wana wa Elazari walikuwa wenye wakuu wengi zaidi kuliko wana wa Itamari; kwa hiyo walipowagawanya, wakatokea kwa wana wa Elazari wakuu wa milango kumi na sita, lakini kwa wana wa Itamari wakuu wa milango wanane tu. Lakini wao kwa wao wakawagawanya kwa kuwapigia kura, kwani walikuwako watambikaji wakuu wa Patakatifu na watambikaji wakuu wa Mungu kwao wana wa Elazari nako kwao wana wa Itamari. Naye Semaya, mwana wa Netaneli, aliyekuwa mwandishi wao Walawi akawaandika, mfalme na wakuu wake na mtambikaji Sadoki na Ahimeleki, mwana wa Abiatari, na wakuu wa milango ya watambikaji na Walawi wakitazama, ikawa hivi: mlango mmoja wa Elazari ukichukuliwa kwa kura, ukachukuliwa nao wa pili, kisha ukachukuliwa nao mmoja wa Itamari. Kura ya kwanza ikamwangukia Yoyaribu, ya 2 Yedaya, ya 3 Harimu, ya 4 Seorimu, ya 5 Malkia, ya 6 Miyamini, ya 7 Hakosi, ya 8 Abia, ya 9 Yesua, ya 10 Sekania, ya 11 Eliasibu, ya 12 Yakimu, ya 13 Hupa, ya 14 Yesebabu, ya 15 Bilga, ya 16 Imeri, ya 17 Heziri, ya 18 Hapisesi, ya 19 Petaya, ya 20 Ezekieli, ya 21 Yakini, ya 22 Gamuli, ya 23 Delaya, ya 24 Mazia. Huu ulikuwa ukuu wao katika utumishi wao wa kuingia nyumbani mwa Bwana kwa matengenezo yao, aliyoyatoa baba yao Haroni, kama Bwana Mungu wa Isiraeli alivyomwagiza. Wale wana wengine wa Lawi ni hawa: Kwa wana wa Amuramu: Subaeli, kwa wana wa Subaeli: Yehedia. Kwake Rehabia: wana wa Rehabia mkuu wao alikuwa Isia. Kwao wa Isihari: Selomoti, kwa wana wa Selomoti: Yahati. Nao wana wa Heburoni walikuwa Yeria, wa pili Amaria, wa tatu Yahazieli, wa nne Yekamamu. Wana wa Uzieli ni Mika, kwa wana wa Mika: Samiri. Ndugu ya Mika alikuwa Isia, kwa wana wa Isia alikuwa Zakaria. Wana wa Merari walikuwa: Mahali na Musi na wana wa Mwanawe Yazia. Wana wa Merari waliokuwa wa mwanawe Yazia ndio Sohamu na Zakuri na Iburi. Wa Mahali alikuwa Elazari asiyekuwa na wana. Wa Kisi ndio wana wa Kisi: Yerameli. Wana wa Musi walikuwa Mahali na Ederi na Yerimoti. Hawa ndio wana wa Lawi kwa milango yao. Wao nao waliwapigia kura sawasawa kama ndugu zao wana wa Haroni, mfalme Dawidi na Sadoki na Ahimeleki na wakuu wa milango ya watambikaji na Walawi wakitazama; aliyekuwa mkuu wa mlango alipigiwa kura sawasawa kama ndugu yake mdogo. Kisha Dawidi na wakuu wa vikosi wakawatenga kwao wana wa Asafu na kwao wa Hemani na kwao wa Yedutuni wao waliolifumbua Neno kwa kupiga mazeze na mapango na matoazi, waje kutumika hivyo. Hesabu yao walioitumikia kazi hiyo ni hii: kwa wana wa Asafu walikuwa Zakuri na Yosefu na Netania na Asarela; hawa wana wa Asafu waliongozwa na Asafu aliyelifumbua Neno kwa kuongozwa na mfalme. Kwa Yedutuni walikuwa wana wa Yedutuni: Gedalia na Seri na Yesaya, Hasabia na Matitia (na Simei), watu sita; hawa waliongozwa kupiga mazeze na baba yao Yedutuni aliyelifumbua Neno kwa kumshukuru na kumtukuza Bwana. Kwa Hemani walikuwa wana wa Hemani: Bukia, Matania, Uzieli, Sebueli na Yerimoti, tena Hanania, Hanani, Eliata, Gidalti na Romamuti-Ezeri, tena Yosibekasa, Maloti, Hotiri, Mahazioti. Hawa wote walikuwa wana wa Hemani aliyekuwa mchunguzaji wa mfalme; kwa hivyo, Mungu alivyomwambia, ya kuwa ataitukuza pembe yake, Mungu alikuwa amempa wana kumi na wanne wa kiume na watatu wa kike. Hawa wote waliongozwa na baba zao kuimba nyumbani mwa Bwana na kupiga matoazi na mapango na mazeze, wakatumika hivyo nyumbani mwa Mungu kwa hivyo, mfalme alivyowaongoza akina Asafu na Yedutuni na Hemani. Walipohesabiwa pamoja na ndugu zao waliofundishwa kumwimbia Bwana, wote walioijua kazi hii walikuwa 288. Wakazipigia zamu zao kura, mdogo sawasawa kama mkubwa, naye mfunzi sawasawa kama mwanafunzi. Hapo kura ya kwanza ya Asafu ikamwangukia Yosefu; ya 2 ikamwangukia Gedalia na ndugu zake na wana wake, pamoja watu 12. Ya 3 Zakuri na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 4 Isiri na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 5 Netania na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 6 Bukia na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 7 Yesarela na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 8 Yesaya na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 9 Matania na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 10 Simei na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 11 Azareli na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 12 Hasabia na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 13 Subaeli na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 14 Matitia na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 15 Yeremoti na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 16 Hanania na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 17 Yosibekasa na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 18 Hanani na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 19 Maloti na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 20 Eliata na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 21 Hotiri na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 22 Gidalti na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 23 Mahazioti na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Ya 24 Romamuti-Ezeri na wana wake na ndugu zake, pamoja watu 12. Mafungu ya walinda malango yalikuwa haya: kwao wa Kora alikuwa Meselemia, mwana wa kore, naye alikuwa mmoja wao wana wa Asafu. Wana wa Meselemia walikuwa wa kwanza Zakaria, wa pili Yediaeli, wa tatu Zebadia, wa nne Yatinieli; wa tano Elamu, wa sita Yohana, wa saba Elihoenai. Wana wa Obedi-Edomu walikuwa wa kwanza Semaya, wa pili Yozabadi, wa tatu Yoa, wa nne Sakari, wa tano Netaneli; wa sita Amieli, wa saba Isakari, wa nane Peultai, kwani Mungu alimbariki. Naye mwanawe Semaya alikuwa amezaliwa wana walioitawala milango yao, kwani walikuwa waume wenye nguvu. Wana wa Semaya walikuwa Otini na Refaeli na Obedi, tena Elizabadi na ndugu zake Elihu na Semakia waliokuwa wenye nguvu. Hawa wote walikuwa miongoni mwao wana wa Obedi-Edomu, wao na wana wao na ndugu zao walikuwa watu wenye nguvu walioufalia huo utumishi; hao wa Obedi-Edomu walikuwa 62. Naye Meselemia alikuwa na wana na ndugu waliokuwa wenye nguvu, nao walikuwa 18. Naye Hosa aliyekuwa mmoja wao wana wa Merari alikuwa na wana, mkuu wao alikuwa Simuri, lakini siye wa kwanza, lakini baba yake alimweka kuwa mkuu; wa pili alikuwa Hilkia, wa tatu Tebalia, wa nne Zakaria. Wana wote wa Hosa pamoja na ndugu zake walikwua 13. Katika haya mafungu ya walinda malango wakuu wao walikuwa na zamu zao za kutumika nyumbani mwa Bwana sawasawa kama ndugu zao. Walipoipigia kura za lango kwa lango, waliwapigia wadogo sawasawa kama wakubwa. Hapo kura ya maawioni kwa jua ikamwangukia Selemia; hata mwanawe Zakaria aliyekuwa mwenye akili za kukata mashauri wakampigia kura, nayo kura yake ikaangukia kaskazini. Ya Obedi-Edomu ikaangukia kusini, nayo ya wanawe ikaiangukia nyumba ya vilimbiko. Ya Supimu na ya Hosa ikaangukia machweoni kwa jua penye lango la Saleketi, ngazi ya kupandia juu ilipo; hapo vilifuatana kilindo na kilindo. Upande wa maawioni kwa jua walikuwa kila siku Walawi sita, kaskazini kila siku wanne, kusini kila siku wanne, napo penye nyumba ya vilimbiko wawili wawili. Penye kijumba kilichojengwa kando upande wa machweoni kwa jua walikuwa wanne penye ngazi, tena wawili hapo penye chumba hicho. Haya ndiyo mafungu ya walinda malango waliokuwa wana wa Kora na wana wa Merari. Kwao Walawi Ahia akawekwa kuviangalia vilimbiko vya nyumba ya Mungu na vilimbiko vitakatifu. Kwao wana wa Ladani ndio wana wa Gersoni, aliowazaa Ladani; waliokuwa wakuu wao hiyo milango ya Ladani, mwana wa Gersoni, ndio wa Yahieli. Wana wa Yehieli, Zetamu na nduguye Yoeli, wakawekwa kuviangalia vilimbiko vya nyumba ya Bwana. Kwao wa Amuramu na kwao wa Isihari na kwao wa Heburoni na kwao wa Azieli ndiko, Sebueli, mwana wa Gersomu, mwana wa Mose, alikokuwa mkuu wao walioviangalia vilimbiko. Tena kwao ndugu zake waliozaliwa na Eliezeri alikuwa mwanawe Rehabia, mwanawe alikuwa Yesaya, mwanawe alikuwa Yoramu, mwanawe alikuwa Zikiri, mwanawe alikuwa Selomiti. Huyu Selomiti na ndugu zake wakawekwa kuviangalia vilimbiko vitakatifu, alivyovitakasa mfalme Dawidi pamoja na wakuu wa milango na wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia na wakuu wa vikosi. Walivitoa katika mateka ya vita, wakavitakasa kuziongeza mali za nyumba ya Bwana. Navyo vyote, alivyovitakasa mtazamaji Samweli na Sauli, mwana wa Kisi, na Abineri, mwana wa Neri, na Yoabu, mwana wa Seruya, vyote pia vikatiwa mikononi mwa Selomiti na ndugu zake. Kwao wa Isihari waliwekwa Kenania na wanawe kufanya kazi za huko nje kwa Waisiraeli, wawe wenye amri na waamuzi wao. Kwao wa Heburoni waliwekwa Hasabia na ndugu zake, watu 1700 wenye nguvu, kuwaangalia Waisiraeli waliokuwako ng'ambo ya huku ya Yordani, upande wa machweoni kwa jua, wafanye kazi zote za Bwana, tena wamtumikie mfalme. Kwao wa Heburoni alikuwa naye Yeria aliyekuwa mkuu wao wa Heburoni kwa vizazi vyao na kwa milango yao; walipohesabiwa katika mwaka wa arobaini wa ufalme wa Dawidi, wakaonekana kwao mafundi wa vita wenye nguvu mle Yazeri wa Gileadi. Nao ndugu zake waliokuwa wenye nguvu, watu 2700, nao walikuwa wakuu wa milango. Hawa mfalme Dawidi aliwaweka kuwaangalia watu wa Rubeni na wa Gadi nao wa nusu ya shina la Manase, wafanye mambo yote ya Mungu na mambo ya mfalme yawapasayo. Hii ndiyo hesabu yao wana wa Isiraeli wakuu wa milango na wakuu wa maelfu na wa mamia nao wenye amri waliomtumikia mfalme katika mambo yote yayapasayo hayo mafungu, wakiingia, tena wakitoka mwezi kwa mwezi miezi yote ya mwaka, nalo fungu moja lilikuwa watu 24000. Mkuu wa fungu la kwanza la mwezi wa kwanza alikuwa Yasobamu, mwana wa zabudieli; nalo fungu lake lilikuwa lenye watu 24000. Alikuwa mmoja wao wana wa Peresi, akawa kichwa chao wakuu wote wa vikosi vya mwezi wa kwanza. Naye mkuu wa fungu la mwezi wa pili alikuwa Mwahohi Dodai, naye mkubwa wa fungu lake alikuwa Mikloti; hata fungu lake lilikuwa lenye watu 24000. Mkuu wa kikosi cha tatu cha mwezi wa tatu alikuwa Benaya, mwana wa mtambikaji Yoyada, yeye alikuwa kichwa, nalo fungu lake lilikuwa lenye watu 24000. Huyu Benaya alikuwa fundi wa vita kwao wale thelathini, naye alikuwa mkuu wao wale thelathini. Aliyeliongoza fungu lake alikuwa mwanawe Amizabadi. Mkuu wa nne wa mwezi wa nne alikuwa Asaheli, ndugu yake Yoabu, naye mwanawe Zebadia alimfuata. Fungu lake nalo lilikuwa lenye watu 24000. Mkuu wa tano wa mwezi wa tano alikuwa mkuu Mwizirahi Samuhuti, fungu lake nalo lilikuwa lenye watu 24000. Mkuu wa sita wa mwezi wa sita alikuwa Ira, mwana wa Ikesi wa Tekoa, fungu lake nalo lilikuwa lenye watu 24000. Mkuu wa saba wa mwezi wa saba alikuwa Mpuloni Helesi aliyekuwa mmoja wao wana wa Efuraimu. Fungu lake nalo lilikuwa lenye watu 24000. Mkuu wa nane wa mwezi wa nane alikuwa Sibekai wa Husa aliyekuwa mmoja wao Wazera. Fungu lake nalo lilikuwa lenye watu 24000. Mkuu wa tisa wa mwezi wa tisa alikuwa Abiezeri wa Anatoti aliyekuwa mmoja wao Wabenyamini. Fungu lake nalo lilikuwa lenye watu 24000. Mkuu wa kumi wa mwezi wa kumi alikuwa Maharai wa Netofa aliyekuwa mmoja wao Wazera. Fungu lake nalo lilikuwa lenye watu 24000. Mkuu wa kumi na moja wa mwezi wa kumi na moja alikuwa Benaya wa Piratoni aliyekuwa mmoja wao wana wa Efuraimu. Fungu lake nalo lilikuwa lenye watu 24000. Mkuu wa kumi na mbili wa mwezi wa kumi na mbili alikuwa Heldai wa Netofa aliyekuwa wa mlango wa Otinieli. Fungu lake nalo lilikuwa lenye watu 24000. Wakuu wa mashina ya Isiraeli walikuwa hawa: kwa Warubeni alikuwa mkubwa Eliezeri, mwana wa zikiri; kwa Wasimeoni Sefatia, mwana wa Maka; kwa Lawi Hasabia, mwana wa Kemueli; kwa Haroni Sadoki; kwa Yuda Elihu aliyekuwa mmoja wao ndugu zake Dawidi; kwa Isakari Omuri, mwana wa Mikaeli; kwa Zebuluni Isimaya, mwana wa Obadia; kwa Nafutali Yerimoti, mwana wa Azirieli; kwa wana wa Efuraimu Hosea, mwana wa Azazia; kwa nusu ya shina la Manase Yoeli, mwana wa Pedaya; kwa nusu ya Manase kule Gileadi Ido, mwana wa Zakaria, tena kwa Benyamini Yasieli, mwana wa Abineri; kwa Dani Azareli, mwana wa Yerohamu. Hawa walikuwa wakuu wa mashina ya Isiraeli. Lakini wao waliokuwa wa miaka ishirini nao wasioipata bado Dawidi hakuwahesabu, kwani Bwana alisema, ya kuwa atawaongeza Waisiraeli, wawe wengi kama nyota za mbinguni. Yoabu, mwana wa Seruya, alianza kuwahesabu, lakini hakumaliza, maana kwa ajili hii mapatilizo makali yaliwapata Waisiraeli. Kwa hiyo hesabu hiyo haikutiwa katika hesabu ya Mambo ya siku za mfalme Dawidi. Mtunza vilimbiko vya mfalme alikuwa Azimaweti, mwana wa Adieli; naye mtunza vilimbiko vilivyokuwa mashambani na mijini na mizabibuni na ngomeni alikuwa Yonatani, mwana wa Uzia. Msimamizi wa wafanya kazi za kulima mashambani alikuwa Eziri, mwana wa Kelubu. Msimamizi wa mizabibu alikuwa Simei wa Rama, naye mtunza mvinyo zilizolimbikwa mizabibuni alikuwa Msifumi Zabudi. Msimamizi wa michekele na wa mikuyu iliyokuwako katika nchi ya tambarare alikuwa Baali-Hanani wa Gaderi, naye mtunza mafuta yaliyolimbikwa alikuwa Yoasi. Msimamizi wa ng'ombe waliolisha Saroni alikuwa Sitirai wa Saroni, naye msimamizi wa ng'ombe walioko mabondeni alikuwa Safati, mwana wa Adilai. Msimamizi wa ngamia alikuwa Mwisimaeli Obili, naye msimamizi wa punda wake alikuwa Yehedia wa Meronoti. Msimamizi wa mbuzi na kondoo alikuwa Mhagri Yazizi. Hawa wote walikuwa watunza mali za mfalme Dawidi. Yonatani, mjomba wake Dawidi, alikuwa mwenye kula njama na mfalme, naye alikuwa mwenye utambuzi na mjuzi wa vitabu. Naye Yehieli, mwana wa Hakemoni, alikuwa mkuza wana wa mfalme. Naye Ahitofeli alikuwa mwenye kula njama na mfalme, naye Mwarki Husai alikuwa rafiki yake mfalme. Waliomfuata Ahitofeli walikuwa Yoyada, mwana wa Benaya, na Abiatari. Mkuu wa vikosi vya mfalme alikuwa Yoabu. Dawidi akawakusanya Yerusalemu wakuu wote wa Waisiraeli, wakuu wa mashina na wakuu wa mafungu yaliyomtumikia mfalme na wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia na wakuu wa mali na wa mapato yote ya mfalme na wanawe pamoja na watumishi wa nyumbani na mafundi wa vita nao wote waliokuwa waume wenye nguvu. Ndipo, mfalme Dawidi alipoinuka, asimame kwa miguu yake, akasema: Nisikilizeni, ninyi ndugu zangu nanyi mlio wa ukoo wangu! Mimi naliwaza moyoni mwangu kujenga nyumba, ndimo Sanduku la Agano la Bwana lipate kutulia, iwe mahali, Mungu wetu awekee miguu yake, nikaitengeneza mijengo. Lakini Mungu akaniambia: Hutalijengea Jina langu nyumba, kwani wewe ni mtu wa kupiga vita, ukamwaga damu. Lakini Bwana Mungu wa Isiraeli alinichagua katika mlango wote wa baba yangu, niwe mfalme wa Waisiraeli kale na kale, kwani alimchagua Yuda, awe mkubwa, namo mlangoni mwa Yuda akauchagua mlango wa baba yangu, namo katika wana wa baba yangu akapendezwa kunifanya mfalme wa Waisiraeli wote. Kisha katika wanangu wote, kwani Bwana akanipa wana wengi, akamchagua mwanangu Salomo, akae katika kiti cha ufalme wa Bwana na kuwatawala Waisiraeli. Akaniambia: Mwanao Salomo ndiye atakayeijenga nyumba yangu na nyua zangu, kwani nimemchagua, awe mwanangu, mimi nami nitakuwa baba yake. Nao ufalme wake nitaushikiza, uwe wa kale na kale, akijishupaza kuyafanya maagizo yangu na maamuzi yangu kama leo. Sasa machoni pao Waisiraeli wote walio mkutano wa Bwana namo masikioni pake Mungu wetu ninawaonya: Yaangalieni na kuyatafuta maagizo yote ya Bwana Mungu wenu, mpate kuishika nchi hii njema, iwe yenu, kisha mwiachie wana wenu watakaokuwa nyuma yenu, iwe fungu lao kale na kale! Nawe mwanangu Salomo, mjue Mungu wa baba yako, umtumikie kwa moyo wote mzima na kwa roho ipendezwayo naye! Kwani Bwana huichungua mioyo yote na kuyatambua mawazo yote, iliyoyatunga. Utakapomtafuta, atakuonekea; lakini ukimwacha, atakutupa kale na kale. Sasa vitazame vema! Kwani Bwana amekuchagua, uijenge nyumba itakayokuwa Patakatifu! Jihimize kuyafanya! Kisha Dawidi akampa mwanawe salomo mfano wa ukumbi na wa nyumba zake na wa vyumba vyake vya vilimbiko na wa vyumba vya juu na wa vyumba vya ndani na wa nyumba ya kupatia upozi, hata mfano wao yote, aliyokuwa ameyawaza rohoni mwake, wa nyua za nyumba ya Bwana na wa vyumba vyote vilivyozizunguka na wa vilimbiko vya nyumba ya Mungu na wa vilimbiko vitakatifu. Akamwambia nazo zamu za watambikaji na za Walawi na kazi zote za utumishi wa nyumbani mwa Bwana na vyombo vyote vya utumishi wa nyumbani mwa Bwana. Akampa nazo dhahabu zilizopimwa; kila chombo kimoja cha kila kazi ya utumishi kilikuwa na dhahabu yake, tena fedha zilizopimwa, kila chombo kimoja cha kila utumishi fedha yake. Hata vinara vilipimiwa dhahabu zao, nazo taa zao dhahabu zao kila kinara kimoja na kila taa moja ilipimiwa dhahabu zake, hata fedha za vinara na za taa zao zilipimiwa kila kinara kimoja, kama kilivyotumika. Akampa nazo dhahabu zilizopimiwa meza za mikate, aliyowekwa Bwana, kila meza dhahabu zake, hata fedha za meza za fedha. Akampa tena dhahabu tupu za nyuma na za vyano na za madumu na za vinyweo vya dahabu, kila kinyweo kimoja kilipimiwa dhahabu zake, navyo vinyweo vya fedha vilipimiwa kila kinyweo kimoja fedha zake. Akampa nazo dhahabu zilizong'azwa za meza ya kuvukizia uvumba, nazo zilipimwa. Kisha akampa mfano wa gari, ndio makerubi ya dhahabu yaliyokunjua mabawa, yalifunike Sanduku la Agano la Bwana, Akamwambia: Haya yote yamo katika mwandiko uliotoka mkononi mwa Bwana, nikaupata, unifundishe kazi zote za mfano huu. Kisha Dawidi akamwambia mwanawe Salomo: Jipe moyo, upate nguvu za kuyafanya! Usiogope, wala usiingiwe na vituko! Kwani Bwana Mungu aliye Mungu wangu atakuwa na wewe, hatakuacha, wala hatakuepuka, hata kazi zote za utumishi wa nyumba ya Bwana zimalizike. Tazama! Yako mafungu ya watambikaji na ya Walawi wa kuufanya utumishi wote wa hiyo nyumba ya Mungu, tena unao mafundi wa kila kazi wanaotaka kukusaidia kwa moyo, nao huujua kweli huo utumishi wote, hata wakuu na watu wote watakutii yote, utakayowaambia. Mfalme Dawidi akauambia ule mkutano wote: Mwanangu Salomo, huyu mmoja, Mungu aliyemchagua, ujana wake ungali mchanga bado, nayo kazi hii ni kubwa, kwani si mtu anayejengewa jumba hili tukufu, ila ni Bwana Mungu. Kwa nguvu zangu zote nimeitengenezea nyumba ya Mungu wangu dhahabu za vyombo vya dhahabu na fedha za vyombo vya fedha na shaba za vyombo vya shaba na vyuma vya vyombo vya chuma na miti ya mijengo, tena vito vya Sardio na vito vyenye dhahabu ukingoni na vito vyeusi na vito vya rangi nyinginenyingine na vito vya kila namna vyenye kima na mawe mengi meupe. Tena kwa kupendezwa na nyumba ya Mungu wangu, dhahabu na fedha zilizo mali zangu nimeitolea nyumba ya Mungu wangu, niziongeze hizo zote, nilizoitengenezea nyumba hiyo takatifu. Vipande vya dhahabu 3000 vya dhahabu ya Ofiri, ndio frasila 9000, na vipande vya fedha zilizong'azwa 7000, ndio frasila 21000 za kuzifunikiza kuta za nyumba. napo panapopaswa na dhahabu papate dhahabu, napo panapopaswa na fedha papate fedha, napo, mafundi watakapozitumia za kazi zo zote. Sasa hivi kwenu yuko nani anayetaka kukijaza mwenyewe kiganja chake, apate kumpa Bwana? Ndipo, wakuu wa milango wa wakuu wa mashina ya Waisiraeli na wakuu wa maelfu na wa mamia nao wakuu wa kazi za mfalme walipochanga kwa kupendezwa, wakatoa vya kutumiwa nyumbani mwa Mungu vipande vya dhahabu 5000, ndio frasila 15000, na robo za dhahabu 10000, ndio shilingi kama 400000, na vipande vya fedha 10000 kumi, ndio frasila 30000, na vipande vya shaba 18000, ndio frasila 54000, na vipande vya chuma 100000 ndio frasila 300000. Nao walioonekana kuwa wenye vito wakavitia katika vilimbiko vya nyumba ya Bwana mkononi mwa Mgersoni Yehieli. Watu wakavifurahia hivyo, walivyovitoa kwa kupenda wenyewe, kwani kila alimtolea Bwana kwa kupenda kwa moyo wote mzima, naye mfalme Dawidi alifurahi na kuona furaha kubwa. Ndipo, Dawidi alipomtukuza Bwana mbele ya mkutano wote, yeye Dawidi akisema: Utukuzwe wewe Bwana Mungu wa baba yetu Isiraeli toka kale hata kale! Wewe Bwana ndiwe mwenye ukuu na uwezo na utukufu na ung'avu na urembo, kwani yote yaliyomo mbinguni na nchini ni yako, Bwana, ndiwe mfalme wao na kichwa chao yote kwa kuwa huko juu. Mali na macheo hutoka kwako, wewe unayatawala yote pia, mkononi mwako zimo nguvu na uwezo, nao mkono wako ndio unaowapatia wote ukubwa na nguvu. Sasa Mungu wetu, sisi tunakushukuru na kulishangilia Jina lako tukufu. Kwani mimi ni mtu gani wao watu wangu ni watu gani, tukijipatia nguvu za kutoa mali kama hizi kwa kupenda wenyewe? Haya yote yametoka kwako, tumeyatoa mkononi mwako, tukakupa tena. Kwani sisi tu wageni mbele yako wanaojikalia tu, kama baba zetu wote, siku zetu za kuwapo huku nchini ni kama kivuli tu kisicho na kingojeo cha kukaa. Bwana Mungu wetu, wingi huu wote wa mijengo yo yote, tuliyoitengeneza ya kulijengea Jina lako takatifu nyumba, umetoka mkononi mwako, kwa maana yote pia ni yako wewe. Ninajua, Bwana, ya kuwa unaijaribu mioyo, ukapendezwa nao wanyokao. Mimi nami kwa hivyo, moyo wangu unavyonyoka, nimeyatoa haya yote kwa kupenda mwenyewe; sasa nao hawa walio ukoo wako waliopo hapa nimewaona na kuwafurahia, ya kuwa wamekutolea mali zao kwa kupenda wenyewe. Bwana Mungu wa baba zetu Aburahamu na Isaka na Isiraeli, yaangalie mambo haya kale na kale kuwa mawazo, walio ukoo wako watakayoyatunga mioyoni mwao, kaishupaze mioyo yao, ikuelekee wewe! Naye mwanangu Salomo mpe moyo usiogawanyika, ayaangalie maagizo yako na mashuhuda yako na maongozi yako, ayafanye yote, alijenge hilo jumba, nililolitengenezea mijengo! Dawidi akauambia huo mkutano wote: Mtukuzeni Bwana Mungu wenu! Ndipo, watu wote wa mkutano walipomtukuza Bwana Mungu wa baba zao na kujiinamisha na kumwangukia Bwana na mfalme. Wakamtolea Bwana ng'ombe za tambiko; kesho yake siku hiyo wakamteketezea Bwana madume ya ng'ombe elfu na madume ya kondoo elfu na wana kondoo elfu pamoja na kumtolea vinywaji vya tambiko na ng'ombe nyingi nyingine za tambiko kwa ajili ya Waisiraeli wote. Wakala, wakanywa mbele ya Bwana siku hiyo na kufurahi sana. Kisha wakamchukua Salomo, mwana wa Dawidi, mara ya pili, awe mfalme wao, wakampaka mafuta, awe mkuu aliye mtu wa Bwana, naye Sadoki wakampaka mafuta, awe mtambikaji. Ndipo, Salomo alipokaa katika kiti cha kifalme cha Bwana, akawa mflame mahali pa baba yake Dawidi, akafanikiwa, nao Waisiraeli wote wakamtii. Hata wakuu wote na mafundi wa vita nao wana wote wa mfalme Dawidi wakajiweka mkononi mwa Salomo, wamtii. Bwana akampatia Salomo ukuu uliozidi machoni pao Waisiraeli wote, akampa hata urembo wa kifalme kuupita wote, walioupata wengine waliokuwa mbele yake wafalme wa Waisiraeli. Dawidi, mwana wa Isai, alikuwa mfalme wa Waisiraeli wote. Nazo siku, alizokuwa mfalme wao Waisiraeli, zilikuwa miaka 40; Heburoni alikaa mwenye ufalme miaka 7, namo Yerusalemu alikaa mwenye ufalme miaka 33. Akafa mwenye miaka mingi alipokuwa ameshiba siku na mali na macheo, naye mwanawe Salomo akawa mfalme mahali pake. Nayo mambo ya mfalme Dawidi, ya kwanza na ya mwisho tunayaona, yameandikwa penye mambo ya mtazamaji Samweli na penye mambo ya mfumbuaji Natani na penye mambo ya mchunguzaji Gadi; ndimo, yalimo mambo yote ya ufalme wake na ya uwezo wake nazo siku zilizompata yeye na Waisiraeli na nchi zote za kifalme. Salomo, mwana wa Dawidi, akajipatia nguvu katika ufalme, naye Bwana Mungu wake akawa naye, akampa ukuu uliozidi. Ndipo, Salomo alipowaita Waisiraeli wote, wakuu wa maelfu na wa mamia na waamuzi na watukufu wa Waisiraeli wote waliokuwa vichwa vya milango, wakaenda, yeye Salomo pamoja na huo mkutano wote, kilimani kwa Gibeoni, kwani ndiko, lilikokuwa Hema la Mkutano la Mungu, Mose, mtumishi wa Bwana, alilolitengeneza nyikani. Lakini Sanduku la Mungu Dawidi alikuwa amelitoa Kiriati-Yearimu, akaliweka hapo, alipolitengenezea yeye Dawidi, kwani alilipigilia hema Yerusalemu. Lakini meza ya shaba ya kutambikia, aliyoitengeneza Besaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwa huko mbele ya Kao lake Bwana; ndiyo, Salomo na mkutano waliyoiendea. Salomo akamtambikia Bwana huko juu ya ile meza ya shaba iliyokuwa penye Hema la Mkutano, akatoa ng'ombe elfu za tambiko za kuteketezwa nzima juu yake hiyo meza. *Usiku huo Mungu akamtokea Salomo, akamwambia: Omba kwangu, uyatakayo, nikupe! Salomo akamwambia Mungu: wewe ulimfanyizia baba yangu Dawidi mambo ya upole mwingi, ukanipa kuwa mfalme mahali pake. Sasa Bwana Mungu, neno lako, ulilomwambia baba yangu Dawidi, na litiwe nguvu, litimie! Kwani wewe umenipa kuwa mfalme wa watu walio wengi kama mavumbi ya nchi. Sasa nipe werevu wa kweli, nipate kujua penye kutoka mbele ya watu hawa na penye kuingia! Kwani mimi ni mtu gani wa kujua kuwaamua hawa watu wengi walio ukoo wako? Ndipo, Mungu alipomwambia salomo: Kwa kuwa jambo kama hili limo moyoni mwako, ukaacha kuniomba mali na mapato mengi na utukufu na kufa kwa wachukivu wako, wala hukuniomba siku nyingi za kuwapo, ila umejiombea werevu wa kweli, upate kujua, jinsi utakavyowaamua walio ukoo wangu, niliokupa, uwe mfalme wao, kwa hiyo umekwisha kupewa werevu wa kweli na ujuzi, tena nitakupa mali na mapato mengi na utukufu, wasioupata wafalme wote waliokuwako mbele yako, nao watakaokuwako nyuma yako hawatayapata.* Kisha Salomo akaondoka kilimani kwa Gibeoni, akaja Yerusalemu akitoka kwenye Hema la Mkutano, akawa mfalme wa Waisiraeli. Salomo akakusanya magari na wapanda farasi, hata akawa na magari 1400 na wapanda farasi 12000, akawakalisha katika miji ya magari namo mwake mfalme mle Yerusalemu. Mfalme akajipatia fedha na dhahabu kuwa nyingi mle Yerusalemu kama mawe, nayo miti ya miangati akajipatia kuwa mingi kama mitamba katika nchi ya tambarare. Nao farasi, Salomo aliokuwa nao, walitoka Misri, wachuuzi wengi wa mfalme waliwaleta wengi wakiwanunua na kuzilipa bei zao. Magari, waliyoyatoa Misri na kuyapeleka kwao, moja lilikuwa fedha 600, na farasi mmoja fedha 150. Vivyo hivyo waliwapelekea nao wafalme wote wa Wahiti na wafalme wa Ushami kwa mikono yao. Salomo akawaza kulijengea Jina la Bwana nyumba, tena kujijengea mwenyewe nyumba ya kifalme. Ndipo, Salomo alipohesabu wachukuzi 70000 na mafundi wa kuchonga mawe 80000, akawapeleka milimani pamoja na wasimamizi wao 3600. Kisha Salomo akatuma watu kwa Huramu, mfalme wa Tiro, kwamba: Kwa hivyo, ulivyopatana na baba yangu Dawidi, ukampelekea miti ya miangati ya kujijengea nyumba ya kukaa humo, tazama, mimi ninataka kulijengea Jina la Bwana Mungu wangu nyumba, niitakase kuwa yake, wavukizie mle mbele yake mavukizo yanukayo vizuri, tena wamwekee mikate siku zote, tena wamtolee ng'ombe za tambiko za asubuhi na za jioni na za siku za mapumziko na za miandamo ya mwezi na za sikukuu za Bwana Mungu wetu, maana hayo ndiyo mazoeo ya Waisiraeli ya kale na kale. Nayo nyumba, nitakayoijenga, sharti iwe kubwa, kwani Mungu wetu ni mkubwa kuliko miungu yote. Lakini yuko nani anayejipatia nguvu ya kumjengea nyumba? Kwani haenei mbinguni, wala mbinguni palipo juu ya mbingu. Mimi nami ni mtu gani nikimjengea nyumba, isipokuwa ya kuvukizia tu mbele yake? Kwa hiyo tuma sasa kwangu mtu aliye fundi kweli wa kutengeneza vyombo kwa dhahabu na kwa fedha na kwa shaba na kwa chuma na kwa nguo za kifalme nyekundu na nyeusi na kwa nguo za rangi, ajuaye hata kuchora machoro pamoja na mafundi walioko kwangu huku Yuda namo Yerusalemu, baba yangu Dawidi aliowaweka. Tena niletee miti ya miangati na mivinje na mininga toka Libanoni, kwani mimi ninajua, ya kuwa watumishi wako hujua kuichonga miti ya Libanoni; nao watu wangu utawaona wa kusaidiana na watu wako, wanitengenezee miti mingi, kwani nyumba, mimi nitakayoijenga, itakuwa kubwa ya ajabu. Tazama, maseremala wanaoichonga miti walio watu wako nitawapa kori 20000, ndio frasila 200000 za ngano na kori 20000, ndio frasila 200000 za mawele na bati 20000, ndio vibaba 700000 vya mvinyo na bati 20000, ndio vibaba 700000 vya mafuta. Huramu, mfalme wa Tiro, akamjibu kwa barua, aliyoituma kwake Salomo kwamba: Kwa hivyo, Bwana anavyoupenda ukoo wake, amekupa kuwa mfalme wao. Huramu akaendelea akisema: Bwana Mungu wa Isiraeli aliyeziumba mbingu na nchi na atukuzwe, kwa kuwa amempa mfalme Dawidi mwana aliye mwerevu wa kweli ajuaye kuzitumia akili na utambuzi, amjengee Bwana nyumba, ajijengee naye nyumba ya kifalme! Sasa natuma kwako mtu aliye fundi kweli, mwenye ujuzi na utambuzi, aliyemfanyia baba yangu Huramu kazi. Ni mwana wa mwanamke wa wana wa kike wa Dani, naye baba yake ni mtu wa Tiro; yeye anajua kutengeneza vyombo kwa dhahabu na kwa fedha na kwa shaba na kwa chuma, kwa mawe na kwa miti, kwa nguo za kifalme nyekundu na nyeusi na kwa nguo za bafta na za rangi, tena anajua kuchora machoro na kutengeneza kazi zote za kifundi, akisaidiwa na mafundi wako na mafundi wa bwana wangu Dawidi. Sasa bwana wangu na awapelekee watumishi wake ngano na mawele, mvinyo na mafuta, aliyoyasema. Nasi tutakata miti huko Libanoni yote, utakayoitaka ya kutumia, kisha tutaipeleka kwako kwa kuieleza baharini hata Yafo (Yope), huko utaichukua kuipeleka Yerusalemu. Ndipo, Salomo alipowahesabu waume wageni wote waliokaa katika nchi, akiifuata njia ya kuhesabu, baba yake Dawidi aliyoishika alipowahesabu, wakaonekana watu 153600. Kwao hao akatoa 70000 kuwa wachukuzi, 80000 kuchonga mawe milimani, 3600 kuwa wasimamizi wa kuwafanyisha watu kazi. Salomo akaanza kuijenga nyumba ya Bwana Yerusalemu katika mlima wa Moriya, Bwana alikomtokea baba yake Dawidi, mahali pale, Dawidi alipopaagiza penye kupuria ngano pa Myebusi Ornani. Akaanza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili wa mwaka wa nne wa ufalme wake. Nayo misingi, Salomo aliyoiweka ya kuijenga nyumba ya Mungu, ni hii: urefu wa kwenda mbele kwa kipimo cha kale ulikuwa mikono 60, nao upana wake ulikuwa mikono 20. Ukumbi uliokuwa mbele ya nyumba ulikuwa mikono 20 kwa kuupatanisha na upana wa nyumba, nao urefu wa kwenda juu ulikuwa mikono 120, ndani akazifunika kuta zake kwa mabati ya dhahabu tupu. Nyumba kubwa akaipigilia kutani mbao za mivinje, nazo akazivika mabati ya dhahabu nzuri, humo namo akachora mitende na mikufu. Akaipamba hiyo nyumba kwa vito vyenye kima, ipate utukufu; zile dhahabu zilikuwa dhahabu za Parawaimu. Boriti na vizingiti na kuta zake na milango yake ya humu nyumbani akaivika mabati ya dhahabu, napo kutani akachora Makerubi. Kisha akapatengeneza Patakatifu Penyewe, urefu wake ulikuwa mikono 20 kwa kuupatanisha na upana wa nyumba, upana wake nao ulikuwa mikono 20, akapavika mabati ya dhahabu nzuri za vipande vya dhahabu 600, ndio frasila 1800. Misumari ilipopimiwa uzito wa dhahabu yao, ukawa sekeli za dhahabu 50, ndio ratli mbili. Navyo vyumba vya juu akavivika dhahabu. Kisha mle Patakatifu Penyewe akatengeneza Makerubi mawili yaliyochongwa na mafundi, nayo akayafunikiza dhahabu. Mabawa ya haya Makerubi urefu wao ulikuwa mikono 20: bawa la moja lenye mikono mitano liligusa ukuta wa nyumba, nalo la pili lenye mikono mitano liligusa bawa la Kerubi la pili; vilevile bawa la Kerubi la pili lenye mikono mitano liligusa ukuta wa nyumba, nalo bawa la pili lenye mikono mitano lilishikamana na bawa lake lile Kerubi jingine. Hivyo, haya mabawa ya Makerubi yalivyokuwa yamekunjuka, yalikuwa yenye mikono 20, nayo yalisimama kwa miguu yao, nazo nyuso zao zilielekea nyumbani. Akatungika pazia la nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na za rangi na za bafta, namo akashonea mifano ya Makerubi. Mbele ya nyumba akaweka nguzo mbili zenye urefu wa mikono 35, nacho kichwa kilichokuwa juu ya kila moja kilikuwa chenye urefu wa mikono mitano. Akatengeneza hata mikufu kuwa ukingo wa chini wa hivyo vichwa, akaitia juu ya hizo nguzo; kisha akatengeneza komamanga 100, akaziangika pale penye mikufu. Akazisimamisha hizo nguzo mbele ya jumba hili, moja kuumeni, moja kushotoni; ya kuumeni akaiita Yakini (Hushikiza), ya kushotoni Boazi (Nguvu imo). Akatengeneza meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko iliyokuwa ya shaba, urefu wake ulikuwa mikono 20, nao upana wake ulikuwa mikono 20, nao urefu wa kwenda juu ulikuwa mikono 10. Akaitengeneza nayo ile bahari kwa shaba zilizoyeyushwa, toka ukingo wake wa huku hata ukingo wake wa huko ilikuwa mikono 10; iliviringana pande zote, urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono 5, nayo kamba ya kuizungusha pande zote ilikuwa ya mikono 30. Chini yake palikuwa na mifano ya ng'ombe iliyoizunguka pande zote pia, kumi kwa mkono mmoja, ikaizunguka hiyo bahari kuwa ukingo wa chini wenye mistari miwili; nayo hii mifano ya ng'ombe ilikuwa imeyeyushiwa mumo humo, bahari ilipoyeyushwa. Ikakaa juu ya ng'ombe 12, tatu zikaelekea kaskazini, tatu zikaelekea baharini, tatu zikaelekea kusini, tatu zikaelekea maawioni kwa jua, nayo bahari ilikuwa juu yao nayo mapaja yao yote yalikuwa yameelekea ndani. Unene wake ulikuwa upana wa shibiri, nao ukingo wake wa juu ulikuwa kama wa kikombe au kama wa ua la uwago. Ndani yake zikaenea bati 3000, ndio pishi 27000. Akatengeneza hata mitungi 10 ya kuoshea, mitano akaweka kuumeni, mitano kushotoni; ndimo, walimosafishia vyombo vilivyotumika katika kazi za kuteketeza ng'ombe za tambiko, lakini bahari ilikuwa yao watambikaji ya kuogea. Akatengeneza hata vinara 10 vya dhahabu sawasawa, kama ilivyoagizwa kuvitengeneza, akaviweka mle jumbani vitano kuumeni, vitano kushotoni. Akatengeneza hata meza 10, akazisimamisha mle jumbani, tano kuumeni, tano kushotoni. Akatengeneza hata vyano 100 vya dhahabu. Kisha akautengeneza ua wa watambikaji na ua mwingine mkubwa na milango ya uani, hii milango akaifunika kwa mabati ya shaba. Ile bahari akaiweka upande wa kuume wa hilo jumba, ielekee mawioni kwa jua, lakini kusini kidogo. Kisha Huramu akatengeneza masufuria na majembe na vyano, akazimaliza kazi, alizomfanyizia mfalme Salomo hapo penye nyumba ya Mungu: nguzo mbili zenya vilemba na vichwa viwili juu ya hizo nguzo na misuko miwili kama ya mkeka ya kuvifunika vile vilemba viwili vilivyoko juu ya hizo nguzo; tena alitengeneza komamanga 400 zilizotiwa katika ile misuko, kila msuko mmoja ukipata mistari miwili ya komamanga ya kuvifunika vile vilemba viwili vya vichwa vilivyoko juu ya hizo nguzo; tena alitengeneza vile vilingo 10, nayo mitungi aliitengeneza iliyowekwa juu ya hivyo vilingo; nayo ile bahari moja na zile ng'ombe 12 zilizokuwa chini yake, nayo masufuria na majembe na nyuma, navyo vyombo vingine vyote Huramu-Abiwu alivitengeneza kwa shaba zilizoyeyushwa, mfalme Salomo avitie nyumbani mwa Bwana. Naye mfalme alikuwa ameagiza kuviyeyusha katika bwawa la Yordani penye udongo mgumu katikati ya miji ya Sukoti na Sereda. Salomo akavitengeneza hivi vyote kuwa vingi mno, kwani shaba zilizotumika hazikupimwa, wala hazikuulizwa, kama ni ngapi. Ndivyo, Salomo alivyovitengeneza vyombo vyote vya kutumiwa nyumbani mwa Mungu, tena meza ya kutambikia iliyokuwa ya dhahabu na meza ya mikate, aliyowekewa Bwana, na vinara pamoja na taa zao zilizokuwa za dhahabu zilizong'azwa, wapate kuziwasha mbele ya Patakatifu Penyewe, kama walivyoagizwa; nayo maua na taa na koleo za dhahabu zilikuwa dhahabu zisizochanganywa na menginemengine; nayo makato ya kusafishia mishumaa na vyano na kata na sinia zilikuwa za dhahabu zilizong'azwa, napo pa kuingia nyumbani ile milango ya ndani pa kupaingilia Patakatifu Penyewe nayo milango ya nyumbani pa kupaingilia Patakatifu ilikuwa ya dhahabu. Kazi zote, ambazo Salomo aliifanyia nyumba ya Bwana zilipomalizika, Salomo akavipeleka vipaji vitakatifu vyote vya baba yake Dawidi pamoja na fedha na dhahabu na vyombo vyote, akaviweka penye vilimbiko vya nyumba ya Mungu. Kisha Salomo akawakusanya wazee wa Waisiraeli nao wote waliokuwa vichwa vya mashina nao wakuu wa milango ya wana wa Isiraeli mle Yerusalemu kwenda kulitoa Sanduku la Agano la Bwana katika mji wa Dawidi ulioitwa Sioni. Ndipo, watu wote wa Isiraeli walipkusanyika kwa mfalme kufanya sikukuu, ikawa mwezi wa saba. Wazee wote wa Isiraeli walipokwisha fika, Walawi wakalichukua hilo Sanduku. Wakalipeleka Sanduku pamoja na Hema la Mkutano na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa Hemani, hivyo watambikaji walio Walawi wakavipandisha. Naye mfalme Salomo pamoja na mkutano wote wa Waisiraeli waliokusanyika kwake mbele ya hilo Sanduku wakatoa mbuzi na kondoo na ng'ombe kuwa ng'ombe za tambiko, nao hawakuhesabika, wala hawakuwangika kwa kuwa wengi mno. Watambikaji wakaliingiza Sanduku la Agano la Bwana mahali pake katika chumba cha ndani kiitwacho Patakatifu Penyewe, wakaliweka chini ya mabawa ya Makerubi. Yale Makerubi yalikuwa yameyakunjua mabawa juu ya mahali pale, Sanduku lilipowekwa; ndivyo, Makerubi yalivyolifunika juu hilo Sanduku nayo mipiko yake. Kwa urefu wa mipiko pembe zao hii mipiko zikaoneka kutoka penye Sanduku kuelekea mle chumbani mwa ndani, lakini nje hazikuoneka; nayo imo humo mpaka siku hii ya leo. Mle Sandukuni hamkuwamo na kitu, ni zile mbao mbili tu, Mose alizozitia huko Horebu, Bwana alipofanya Agano na wana wa Isiraeli, walipotoka Misri. Kisha watambikaji wakatoka Patakatifu; nao hawa watambikaji waliooneka hapo walikuwa wamejitakasa wote pasipo kuziangalia zamu zao, nao waimbaji wote pia walio Walawi, wale wa Asafu na wa Hemani na wa Yedutuni pamoja na wana wao na ndugu zao, wote walikuwa wamevaa nguo za bafta, wakashika patu na mapango na mazeze, wakawa wamesimama upande wa maawioni kwa jua penye meza ya kutambikia, tena walikuwako pamoja na watambikaji 120 wenye kupiga matarumbeta. Palipotukia pa kupigia matarumbeta na kuimba nyimbo, ikawapasa wote kuzisikiza sauti zao kwa mara moja kuwa kama mtu mmoja tu, wamshangilie Bwana na kumshukuru wakipaza sauti na kupiga matarumbeta na patu na vyombo vyote vya kuimbia, wamshangilie Bwana, ya kuwa ni mwema, ya kuwa upole wake ni wa kale na kale. Ndipo, Nyumbani mlipojaa wingu, humo Nyumbani mwa Bwana. Nao watambikaji hawakuweza kusimama humo na kuzifanya kazi za utumishi wao kwa ajili ya hilo wingu, kwani utukufu wa Bwana uliijaza Nyumba ya Mungu. Ndipo, Salomo aliposema: Bwana alisema, ya kuwa hukaa mawinguni mwenye weusi. Nami nimekujengea Nyumba ya kukaa, iwe Kao lako la kukaa humu kale na kale. Kisha mfalme akaugeuza uso wake, akaubariki mkutano wote wa Waisiraeli, nao wote wa mkutano wa Waisiraeli walikuwa wamesimama. Akasema: Atukuzwe Bwana Mungu wa Isiraeli! Aliyomwambia baba yangu Dawidi kwa kinywa chake, ameyatimiza kwa mikono yake, ya kwamba: Tangu siku ile, nilipowatoa walio ukoo wangu katika nchi ya Misri, sikuchagua mji katika mashina yote ya Isiraeli, ndimo wanijengee Nyumba, Jina langu likae humo, wala sikuchagua mtu wa kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli. Kisha nikachagua Yerusalemu, Jina langu liwemo, nikamchagua Dawidi wa kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli. Baba yangu Dawidi akawaza moyoni kulijengea Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli nyumba, lakini Bwana akamwambia baba yangu Dawidi: Ukiwaza moyoni mwako kulijengea Jina langu nyumba, umefanya vema kuyawaza hayo moyoni mwako. Lakini wewe hutaijenga hiyo nyumba, kwani mwanao atakayetoka viunoni mwako ndiye atakayelijengea Jina langu nyumba. Bwana akalitimiza hilo neno, alilolisema, nami nikaondokea mahali pa baba yangu Dawidi, nikakaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli, kama Bwana alivyosema, nikalijengea Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli Nyumba hii. Nikaliweka humu Sanduku, Agano la Bwana lilimo, alilolifanya na wana wa Isiraeli. Kisha akaja kusimama mbele ya meza ya kumtambikia Bwana machoni pao mkutano wote wa Waisiraeli, akaikunjua mikono yake. Kwani Salomo alikuwa ametengeneza hapo ulingo wa shaba, akauweka hapo uani katikati, urefu wake ulikuwa mikono mitano, nao upana wake mikono mitano, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono mitatu, akasimama hapo juu, akayapiga magoti yake machoni pao mkutano wote wa Waisiraeli, akaikunjua mikono yake na kuielekeza mbinguni, akasema: Bwana Mungu wa Isiraeli, hakuna Mungu afananaye na wewe, wala mbinguni wala nchini. Unawashikia watumishi wako agano lako na upole wako, wakiendelea mbele yako kwa mioyo yao yote. Umemshikia mtumishi wako, baba yangu Dawidi, uliyomwambia; uliyoyasema kwa kinywa chako, umeyatimiza kwa mkono wako, kama inavyoonekana siku hii ya leo. Na sasa Bwana Mungu wa Isiraeli, mshikie mtumishi wako, baba yangu Dawidi, uliyomwambia kwamba: Kwako hakutakoseka mtu atakayekaa machoni pangu katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli, wanao wakiziangalia tu njia zao, waendelee kuyafuata Maonyo yangu, kama wewe ulivyoendelea kuwa machoni pangu. Sasa Bwana Mungu wa Isiraeli, hilo neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Dawidi, na lishupazwe! Inakuwaje? Mungu anakaa kweli na watu huku nchini? Tazama! Mbingu nazo mbingu zilizoko juu ya mbingu hazikuenei, sembuse Nyumba hii, niliyoijenga! Yageukie maombo ya mtumishi wako na malalamiko yake, Bwana Mungu wangu, uvisikilize vilio na maombo, mtumishi wako anayokuomba usoni pako! Uwe macho kuiangalia Nyumba hii mchana na usiku, ipate kuwa mahali pale, uliposema: Mahali hapa ndipo, Jina langu litakapokuwa! Kwa hiyo yasikie maombo, mtumishi wako atakayokuomba mahali hapa! Yasikie nayo malalamiko ya mtumishi wako nayo yao walio ukoo wako wa Waisiraeli, watakayokuomba mahali hapa! Wewe wasikie huko juu mbinguni, unakokaa! Tena utakapowasikia uwaondolee makosa! Mtu akikosana na mwenziwe, akachukuliwa, aape, basi, wakimwapisha hivyo, naye akija kuapia mbele ya meza ya kutambikia katika Nyumba hii, wewe umsikie huko mbinguni, ulitengeneze jambo hilo na kuwaamua watumishi wako, ukimrudishia yule aliyekosa na kumtwika kichwani pake matendo yake, tena yule asiyekosa ukimtokeza kuwa pasipo kosa, ukimpa yaliyo haki yake. Itakuwa, walio ukoo wako wa Waisiraeli wakimbizwe na adui, kwa kuwa wamekukosea; kisha watakapokurudia na kuliungama Jina lako, wakuombe na kukulalamikia humu Nyumbani, wewe na uwasikie huko mbinguni, uwaondolee walio ukoo wako wa Waisiraeli makosa yao! Kisha warudishe katika nchi hii, uliyowapa baba zao. Itakuwa, mbingu zizibane, mvua isinye, kwa kuwa wamekukosea; kisha watakapoombea mahali hapa na kuliungama Jina lako na kuyaacha makosa yao, kwa kuwa umewatesa, wewe na uwasikie huko mbinguni, uwaondolee makosa yao walio watumishi wako nayo yao walio ukoo wako wa Waisiraeli! Kisha wafundishe njia iliyo njema, waishike, upate kuinyeshea nchi yako mvua tena, kwa kuwa umeipa watu wa ukoo wako, iwe fungu lao. Itakuwa, njaa iingie katika nchi hii au magonjwa mabaya, itakuwa, jua kali linyaushe mashamba yote, itakuwa, nzige na funutu wamalize vilaji vyote, itakuwa, adui zao wawasonge watu kwao malangoni mwao, itakuwa, mapigo menginemengine na magonjwa yo yote yawapate, basi, lisikie kila ombo na kila lalamiko litakalokutokea, kama ni la mtu awaye yote, au la watu wote walio ukoo wako wa Waisiraeli, kwa kuwa kila mtu anayajua mapigo yake na maumivu yake! Hapo, watakapokuja kuikunjua mikono yao humu Nyumbani, wewe na uwasikie huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa, uwaondolee makosa na kumrudishia kila mtu, kama njia zake zilivyo, kwa hivyo, unavyoujua moyo wake! Kwani wewe peke yako unaijua mioyo ya wana wa watu, kusudi wakuogope na kuzishika njia zako siku zote, watakazokuwapo katika nchi hii, uliyowapa baba zetu. Tena itakuwa, hata mgeni asiye wa ukoo wako wa Waisiraeli aje huku na kutoka katika nchi ya mbali kwa ajili ya Jina lako lililo kuu na kwa ajili ya kiganja chako kilicho na nguvu na kwa ajili ya mkono wako uliokunjuka; basi, hapo watakapokuja, waombee humu Nyumbani, wewe na uwasikie huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa, uyafanye yote, yule mgeni atakayokuomba na kukulilia, makabila yote ya nchi yalijue Jina lako, wakuogope kama wao walio ukoo wako wa Waisiraeli, tena wajue, ya kuwa Nyumba hii, niliyoijenga, imeitwa kwa Jina lako. Itakuwa, walio ukoo wako wakitoka kupigana na adui zao na kuishika njia, utakayowatuma, wakuombe njiani na kuuelekea mji huu, uliouchagua, hata Nyumba hii, niliyolijengea Jina lako, basi, hapo na uyasikie huko mbinguni maombo yao na malalamiko yao, uwatengenezee shauri lao. Tena itakuwa, wakukosee, kwani hakuna mtu asiyekosa, nawe utawakasirikia, uwatie mikononi mwao adui, wawateke na kuwahamisha wakiwapeleka katika nchi ya mbali au ya karibu; lakini hapo, watakapojirudia wenyewe mioyoni mwao katika nchi hiyo, walikohamishiwa, basi, hapo watakapokulalamikia tena katika nchi ya uhamisho wao na kusema: Tumekosa, tumekora manza, tumefanya maovu, watakapokurudia hivyo kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote katika nchi ya uhamisho wao, walikohamishiwa, watakapokuomba na kuielekea nchi yao, uliyowapa baba zao, na mji, uliouchagua, na Nyumba hii, niliyolijengea Jina lako, basi, wewe huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa na uyasikie maombo yao na malalamiko yao, uwatengenezee shauri lao na kuwaondolea walio ukoo wako makosa yao, waliyokukosea! Sasa Mungu wangu, uwe macho, nayo masikio yako yawe yametegwa kuyasikiliza maombo ya mahali hapa! Sasa inuka, Bwana Mungu, uingie hapa, ndipo utulie na Sanduku lililo na nguvu yako! Watambikaji wako, Bwana Mungu, na wavikwe wokovu, nao wakuchao wayafurahie mema! Bwana Mungu, usikatae kuuona uso wa mtu wako aliyepakwa mafuta! Yakumbuke nayo matendo ya upole ya mtumishi wako Dawidi! Salomo alipokwisha kuomba, ndipo, moto uliposhuka toka mbinguni, ukala ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima na ng'ombe nyingine za tambiko, kisha utukufu wa Bwana ukajaa mle Nyumbani. Kwa hiyo watambikaji hawakuweza kuingia Nyumbani mwa Bwana, kwa kuwa utukufu wa Bwana ulijaa Nyumbani mwa Bwana. Nao wana wote wa Isiraeli walipoona, jinsi moto ulivyoshuka nao utukufu wa Bwana ulivyokaa juu ya Nyumba hii, wakapiga magoti na kujinamisha chini hapo palipopigiliwa mawe, wakamwangukia Bwana na kumshukuru, ya kuwa ni mwema, ya kuwa upole wake ni wa kale na kale. Kisha mfalme na mkutano wote wa watu wakamtolea Bwana ng'ombe za tambiko. Mfalme Salomo akatoa ng'ombe 22000 na mbuzi na kondoo 120000 kuwa ng'ombe za tambiko. Ndivyo, mfalme na watu wote walivyoieua Nyumba ya Mungu. Watambikaji wakawa wakisimama na kuziangalia kazi zao, nao Walawi wakashika vyombo vya kumwimbia Bwana, mfalme Dawidi alivyovitengeneza hapo, alipomshangilia Bwana, navyo vikamshukuru Bwana kwamba: Upole wake ni wa kale na kale; nao watambikaji waliowaelekea wakapiga matarumbeta, nao Waisiraeli wote walikuwa wamesimama. Ndipo, Salomo alipokitakasa kipande cha kati cha ua uliokuwa mbele ya Nyumba ya Bwana, kwani ndiko, alikotolea ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na mafuta ya ng'ombe za tambiko za shukrani, kwani ile meza ya shaba ya kutambikia, Salomo aliyoitengeneza, haikuweza kuzieneza ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na vilaji vya tambiko na mafuta ya ng'ombe nyingine za tambiko. Ndivyo, Salomo alivyofanya wakati huo sikukuu ya siku saba, yeye pamoja nao Waisiraeli wote, wakawa mkutano mkubwa sana wa watu waliotoka Hamati mpaka kwenye mto wa Misri. Siku ya nane wakakusanyika tena kufanya sikukuu; kwani zile siku saba ndizo, walizoieneza meza ya kutambikia ng'ombe za tambiko, hii sikukuu nayo ikawa ya siku saba tena. Siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa saba akawapa watu ruhusa kwenda mahemani kwao, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema, Bwana aliomfanyizia Dawidi naye Salomo nao walio ukoo wake wa Waisiraeli. Salomo alipoimaliza Nyumba ya Bwana na nyumba ya mfalme na kufanikiwa yote, yeye Salomo aliyokuwa nayo moyoni ya kufanya Nyumbani mwa Bwana namo nyumbani mwake, ndipo, Bwana alipomtokea Salomo usiku, akamwambia: Nimeyasikia maombo yako, napo mahali hapa nimepachagua, pawe Nyumba ya kunitambikia. Itakuwa, nizizibe mbingu, mvua isinye, au niagize nzige, waile nchi hii, au nitume magonjwa mabaya kwao walio ukoo wangu, basi, wao walio ukoo wangu, walioitwa kwa Jina langu, watakaponyenyekea na kuniomba wakiutafuta uso wangu, warudi na kuziacha njia zao mbaya, ndipo, nitakapowasikia huko mbinguni, niwaondolee makosa yao, niiponye hii nchi yao. Tangu sasa macho yangu yatakuwa wazi, nayo masikio yangu yatakuwa yametegwa kuyasikiliza, watakayoniomba mahali hapa. Sasa nimeichagua Nyumba hii, nikaitakasa, Jina langu lipate kuwa humu kale na kale, nayo macho yangu na moyo wangu yatakuwa humu siku zote. Wewe nawe ukiendelea kuwa machoni pangu, kama baba yako Dawidi alivyoendelea, uyafanye yote, niliyokuagiza, ukiyaangalia maongozi yangu na maamuzi yangu, ndipo, nitakapokisimamisha kiti cha kifalme cha ufalme wako, kama nilivyomwagia baba yako Dawidi kwamba: Kwako hakutakoseka mtu atakayewatawala Waisiraeli. Lakini ninyi mtakaporudi nyuma, myaache maagizo yangu na maongozi yangu, niliyoyatoa machoni penu, mkaja kutumikia miungu mingine na kuiangukia, ndipo, nitakapowang'oa katika hii nchi yangu, niliyowapa, nayo Nyumba hii, niliyoitakasa kuwa Kao la Jina langu, nitaitupa, macho yangu yasiione tena, nitaitoa kuwa fumbo na simango kwa makabila yote. Nayo Nyumba hii iliyokuwa imetukuka kabisa, basi, kila atakayepita hapo ataistukia na kuuliza: Kwa sababu gani Bwana ameifanyizia hivi nchi hii na Nyumba hii? Ndipo, watakapojibu: Kwa kuwa walimwacha Bwana Mungu wa baba zao aliyewatoa katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiangukia na kuitumikia, hii ndiyo sababu, akiwaletea haya mabaya yote. Ile miaka ishirini, ambayo Salomo aliijenga Nyumba ya Bwana na nyumba yake, ilipokwisha, ndipo, Salomo alipoijenga ile miji, Huramu aliyompa Salomo, akakalisha humo wana wa Isiraeli. Kisha Salomo akaenda Hamati-Soba, akauchukua. Akajenga Tadimori ulioko nyikani, hata miji yote yenye vilimbiko, aliyoijenga kule Hamati. Kisha akajenga Beti-Horoni wa juu na Beti-Horoni wa chini kuwa miji yenye maboma iliyokuwa na kuta na malango na makomeo. Ndivyo, alivyojenga hata Balati na miji yote yenye vilimbiko, Salomo aliyokuwa nayo, hata miji yote ya magari na miji ya farasi na majengo yote yaliyompendeza Salomo, aliyotaka kuyajenga kwa mapenzi yake mle Yerusalemu nako huko Libanoni na katika nchi yo yote ya ufalme wake. Watu aliowatumia, ndio wote waliosalia na Wahiti na wa Waamori na wa Waperizi na wa Wahiwi na wa Wayebusi wasiokuwa wa Waisiraeli; wana wao wale waliosalia na kuachwa na wenzao katika nchi hii, kwa kuwa wana wa Isiraeli hawakuwamaliza, basi, hao wote Salomo akawafanyisha kazi za utumwa hata siku hii ya leo. Lakini wana wa Isiraeli Salomo hakuwataka kuwa watumwa wa kumfanyizia kazi, kwani hawa walikuwa wapiga vita na wakuu wa thelathini na wakuu wa magari yake na wapanda farasi wake. Nao wakuu wa mfalme Salomo waliowekwa kusimamia kazi walikuwa 250, ndio waliowatawala watu wa kazi, Binti Farao Salomo akamtoa mjini mwa Dawidi, akampeleka kukaa katika nyumba, aliyomjengea, kwani alisema: Mwanamke asikae kwangu nyumbani mwa Dawidi, mfalme wa Waisiraeli, kwa kuwa ni takatifu, kwani Sanduku la Bwana liliingia mumo humo. Tangu hapo ndipo, Salomo alipomtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa hapo mezani pa kumtambikia Bwana, alipopajenga mbele ya ukumbi; akatoa ng'ombe za tambiko zipasazo kila siku moja, kama Mose alivyoagiza: za mapumziko, za miandamo ya mwezi, za sikukuu zilizo tatu za kila mwaka: sikukuu ya Mikate isiyochachwa, sikukuu ya Majuma na sikukuu ya Vibanda. Kama baba yake Dawidi alivyoviagiza, akayaweka mafungu ya watambikaji ya kuzifanya kazi zao nayo ya Walawi kwa zamu zao: wa kuimba mashangilio nao wa kuwatumikia watambikaji, kama ilivyopasa kila siku moja; akawaweka nao walinda malango kwa mafungu yao, walingoje kila lango moja, kama Dawidi aliyekuwa mtu wa Mungu alivyoviagiza. Hawakutangua agizo la mfalme, alilowaagiza la watambikaji na la Walawi kwa ajili ya mambo yote, hata kwa ajili ya vilimbiko. Kwa hiyo kazi zote za Salomo zikaendelea vema tangu siku ile, misingi ya Nyumba ya Bwana ilipowekwa, hata siku hiyo, Nyumba yote nzima ya Bwana ilipomalizika. Kisha Salomo akaenda Esioni-Geberi na Eloti huko pwani kwenye bahari iliyoko katika nchi ya Edomu. Huramu akatuma kwake vyombo vilivyopelekwa na watumishi wake pamoja na watumishi walioyajua mambo ya baharini; wakaenda Ofiri pamoja na watumishi wake Salomo, wakachukua huko vipande vya dhahabu 450, ndio frasila 1350, wakampelekea mfalme salomo. Mfalme wa kike wa Saba alipousikia uvumi wa Salomo, akaenda Yerusalemu kumjaribu Salomo kwa maulizo ya kufumbafumba, akaja na vikosi vikubwa mno na ngamia waliochukua uvumba na dhahabu nyingi na vito. Alipofika kwa Salomo akasema naye na kumwuliza yote, aliyokuwa nayo moyoni mwake. Salomo akamwelezea yote, aliyomwuliza, halikuwako neno lililofichika maana kwake Salomo, asiloweza kumwelezea. Ndipo, mfalme wa kike wa Saba alipouona werevu wa Salomo kuwa wa kweli, kisha akaitazama nyumba, aliyoijenga, na vilaji vilivyopo mezani na vikao vya watumwa wake na kazi za watumishi wake na mavazi yao, hata watunza vinywaji wake na mavazi yao na dari, aliyoiweka juu ya Nyumba ya Bwana; ndipo, roho yake ilipozimia, akamwambia mfalme: Kumbe ni ya kweli, niliyoyasikia katika nchi yangu ya mambo yako na ya werevu wako ulio wa kweli! Lakini sikuyaitikia hayo maneno yao kuwa ya kweli, mpaka nikija, nikayaona kwa macho yangu. Tena naona, ya kuwa sikuambiwa nusu tu ya werevu wako mwingi mno ulio wa kweli, maana ni mkuu kuliko ule uvumi, niliousikia. Wenye shangwe ni watu wako, nao hawa watumwa wako ni wenye shangwe kwa kusimama mbele yako siku zote na kuyasikia maneno ya werevu wako ulio wa kweli. Bwana Mungu wako na atukuzwe, kwa kuwa alipendezwa na wewe, akakukalisha katika kiti chake cha kifalme, uwe mfalme wa Bwana Mungu wako! Kwa kuwa Mungu wako anawapenda Waisiraeli, awapatie kuwapo kale na kale, alikupa kuwa mfalme wao, uwaamue kwa wongofu. Kisha akampa mfalme vipande vya dhahabu 120, ndio frasila 360, na uvumba mwingi sana na vito; uvumba mwingi kama huo, mfalme wa kike wa Saba aliompa Salomo, ulikuwa haujapatikana bado. Kweli nao watumishi wa Huramu na watumishi wa Salomo waliotoa dhahabu kule Ofiri wakaleta nayo miti ya uvumba na vito, naye mfalme akaitumia hiyo miti ya uvumba ya kutengeneza vipago vya Nyumba ya Bwana na vya nyumba ya mfalme na mazeze na mapango ya waimbaji. Lakini mali kama hizo hazijaonekana siku za mbele katika nchi ya Yuda. Kisha mfalme Salomo akampa mfalme wa kike wa Saba yote, aliyopendezwa nayo, aliyomwomba, kuliko yale, aliyomletea mfalme; kisha akarudi kwenda kwao katika nchi yake, yeye na watumishi wake. Uzito wa dhahabu, Salomo alizoletewa katika mwaka mmoja ulikuwa vipande vya dhahabu 666, ndio frasila 2000, pasipo zile, watembeaji na wachuuzi walizomletea; nao wafalme wote wa nchi ya Waarabu na watawala nchi wakamletea Salomo dhahabu na fedha. Mfalme Salomo akatengeneza ngao 200 za dhahabu zilizofuliwa, kila ngao moja ikatumiwa sekeli 600, ndio nusu kubwa ya frasila ya dhahabu zilizofuliwa. Kisha akatengeneza ngao ndogo 300 za dhahabu zilizofuliwa, hizi ngao ndogo kila moja ikatumiwa sekeli 300, ndio ratli tisa za dhahabu; mfalme akaziweka katika nyumba ya mwituni kwa Libanoni. Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme cha pembe za tembo, akakifunikiza dhahabu tupu. Hicho kiti cha kifalme kilikuwa na vipago sita vya kukipandia, tena hapo chini yake palikuwa pamefanyizwa pa kuwekea miguu, napo palikuwa pa dhahabu. Tena hapo pa kukalia palikuwa na maegemeo huku na huko, nayo mifano miwili ya simba ilikuwa imesimama hapo penye maegemeo. Tena mifano kumi na miwili ya simba ilikuwa imesimama juu ya vile vipago sita huku na huko. Kitu kilichotengenezwa vizuri hivyo hakikuwako katika ufalme wote. Navyo vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Salomo vilikuwa vya dhahabu, navyo vyombo vyote vya ile nyumba ya mwituni kwa Libanoni vilikuwa vya dhahabu zilizong'azwa; kwani fedha ziliwaziwa kuwa si kitu katika siku za Salomo. Kwani merikebu za mfalme zilikwenda Tarsisi zikipelekwa na watumishi wa Huramu; kila miaka mitatu hizo merikebu zilizokwenda Tarsisi zikaja mara moja, zikaleta dhahabu na fedha na pembe za tembo na tumbili na madege wenye manyoya mazuri mno wanaoitwa tausi. Hivyo ndivyo, mfalme Salomo alivyokuwa mkuu kuwapita wafalme wote wa huku nchini kwa utukufu na kwa werevu wa kweli. Wafalme wote wa huku nchini wakataka kuuona uso wake Salomo, wayasikie maneno ya werevu wake wa kweli, Mungu alioutia moyoni mwake. Nao wakaleta kila mtu matunzo yake: vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu na mavazi na mata na uvumba na farasi na nyumbu; vikawa hivyo mwaka kwa mwaka. Salomo akawa na majozi ya farasi 4000 na magari, tena wapanda farasi 12000, akawakalisha katika miji ya magari namo mwake mfalme mle Yerusalemu. Akawa akiwatawala wafalme wote toka lile jito mpaka nchi ya Wafilisti kuifikilia nayo nchi ya Misri. Mfalme akajipatia fedha kuwa nyingi mle Yerusalemu kama mawe, nayo miti ya miangati akajipatia kuwa mingi kama mitamba katika nchi ya tambarare. Wakamletea Salomo farasi, waliowatoa Misri na katika nchi zote. Mambo mengine ya Salomo ya kwanza na ya mwisho hayakuandikwa kwenye mambo ya mfumbuaji Natani na kwenye ufumbuaji wa Ahia wa Silo na kwenye maono ya mchunguzaji Yedi, aliyomchunguzia Yeroboamu, mwana wa Nebati? Salomo akawa mfalme mle Yerusalemu na kuwatawala Waisiraeli wote miaka 40. Kisha Salomo akaja kulala na baba zake, wakamzika mjini mwa baba yake Dawidi, naye mwanawe Rehabeamu akawa mfalme mahali pake. Rehabeamu akaenda Sikemu, kwani Waisiraeli wote walifikia Sikemu kumpa ufalme. Naye Yeroboamu, mwana wa Nebati, alikuwa huko Misri, alikokimbilia alipomkimbia mfalme Salomo; lakini alipopashwa hizo habari akarudi toka Misri. Wakamwita, naye akaja na Waisiraeli wote, wakamwambia Rehabeamu kwamba: Baba yako alitutwisha mzigo mzito, sasa wewe utupunguzie ule utumwa mgumu wa baba yako nao mzigo wake mzito, aliotutwisha! Kisha tutakutumikia. Akawaambia: Kwanza nendeni siku tatu, kisha rudini kwangu! Watu walipokwenda zao, mfalme Rehabeamu akafanya shauri na wazee waliomtumikia baba yake Salomo, alipokuwa mzima bado, akawauliza: Ninyi shauri lenu ni nini? Watu hawa tuwape majibu gani? Wakamwambia hivi: Ukijulikana kwao watu hawa kuwa mwema, ukiwapendeza na kuwaambia maneno mema, ndipo, watakapokuwa watumishi wako siku zote. Lakini akaliacha shauri la wazee, walilompa, akafanya shauri na vijana waliokua naye na kumtumikia, akawauliza: Ninyi shauri lenu ni nini? Tuwape majibu gani watu hawa walioniambia: Tupunguzie mzigo, aliotutwisha baba yako? Vijana hawa waliokuwa naye wakasemezana naye kwamba: Haya ndiyo, uwaambie watu waliokuambia kwamba: Baba yako aliukuza mzigo wetu kuwa mzito, wewe utupunguzie huu mzigo wetu, basi, uwaambie hivyo: Kidole changu kidogo na kinenepe kuliko viuno vya baba yangu; sasa vitakuwa hivi: kama baba yangu aliwatwisha mzigo mzito, mimi nitauzidisha mzigo wenu; kama baba yangu aliwapiga fimbo, mimi nitawapiga viboko vyenye miiba. Yeroboamu na watu wote wakaja kwake Rehabeamu siku ya tatu, kama mfalme alivyosema kwamba: Rudini siku ya tatu! Ndipo, mfalme alipowapa majibu magumu, yeye Rehabeamu akiliacha shauri la wazee, akasema nao na kulifuata shauri la vijana, akawaambia: kama baba yangu aliwatwisha mzigo mzito, mimi nitauzidisha; kama baba yangu aliwapiga fimbo, mimi nitawapiga viboko vyenye miiba. Mfalme hakuwasikia wale watu, kwani Mungu aliyageuza kuwa hivyo, yeye Bwana apate kulitimiza neno lake, alilomwambia Yeroboamu, mwana wa Nebati, kinywani mwa Ahia wa Silo. Waisiraeli wote walipoona, ya kuwa mfalme hakuwasikia, ndipo, watu walipomjibu mfalme kwamba: Sisi tuna bia gani na Dawidi? Hatuna fungu lo lote kwake mwana wa Isai. Waisiraeli, haya! Rudini sasa mahemani kwenu, kila mtu kwake! Nawe Dawidi, na uuangalie mwenyewe mlango wako! Ndipo, Waisiraeli wote walipokwenda mahemani kwao. Ni wana wa Isiraeli waliokaa katika miji ya Yuda tu, Rehabeamu aliowapata, awe mfalme wao. Mfalme Rehabeamu alipomtuma Hadoramu aliyekuwa msimamizi wa kazi za nguvu, wana wa Isiraeli wakampiga mawe, hata akafa. Kisha mfalme Rehabeamu akajihimiza kupanda garini na kukimbilia Yerusalemu. Ndivyo, Waisiraeli walivyojitenga na mlango wa Dawidi mpaka siku ya leo. Rehabeamu alipofika Yerusalemu, akaikusanya milango ya Yuda na ya Benyamini, watu 180000 waliochaguliwa kupiga vita, wapigane na Waisiraeli, wamrudishie Rehabeamu ufalme huo. Lakini neno la Bwana likamjia Semaya aliyekuwa mtu wa Mungu, kwamba: Mwambie Rehabeamu, mwana wa Salomo, mfalme wa Wayuda, nao Waisiraeli wote walioko katika nchi ya Yuda na ya Benyamini kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msipande kwenda kupigana na ndugu zenu! Rudini kila mtu nyumbani kwake! Kwani jambo hili limefanywa na mimi. Walipoyasikia maneno haya ya Bwana wakarudi wakiacha kumwendea Yeroboamu. Rehabeamu alipokaa Yerusalemu akajenga miji yenye maboma katika nchi ya Yuda. Akajenga maboma Beti-Lehemu na Itamu na Tekoa, na Beti-Suri na Soko na Adulamu, na Gati na Maresa na Zifu, na Adoraimu na Lakisi na Azeka, na Sora na Ayaloni na Heburoni; hii ndiyo miji yenye maboma katika nchi ya Yuda na ya Benyamini. Haya maboma akayajenga kuwa yenye nguvu, akaweka humo wenye amri na vilimbiko vya vilaji na vya mafuta na vya mvinyo. Humo katika kila mji mmoja akaweka ngao na mikuki, akaijenga kuwa yenye nguvu nyingi mno. Nchi ya Yuda na ya Benyamini ikawa yake. Watambikaji na Walawi katika nchi zote za Isiraeli wakarudi upande wake na kutoka katika mipaka yao yote. Kwani Walawi wakayaacha malisho na mapato yao, wakaenda Uyuda na Yerusalemu, kwa kuwa Yeroboamu na wanawe waliwatupa, waiswe watambikaji wa Bwana. Akajiwekea mwenyewe watambikaji wa kutambika vilimani, nao wa kutambikia mashetani na ndama, alizozitengeneza. Katika mashina yote ya Isiraeli watu waliojipa mioyo ya kumtafuta Bwana Mungu wa Isiraeli wakawafuata wale, wakaja Yerusalemu kumtolea Bwana Mungu wa baba zao ng'ombe za tambiko. Hawa ndio walioutia ufalme wa Yuda nguvu, wakamwongezea Rehabeamu, mwana wa Salomo, uwezo miaka mitatu, kwani waliendelea katika njia za Dawidi na za Salomo miaka mitatu. Rehabeamu akamwoa Mahalati wa Yerimoti, mwana wa Dawidi na wa Abihaili, binti Eliabu, mwana wa Isai. Huyu akamzalia wana hawa: Yeusi na Semaria na Zahamu. Kisha akamwoa Maka, binti Abisalomu; huyu alimzalia Abia na Atai na Ziza na Selomiti. Rehabeamu akampenda maka, binti Abisalomu, kuliko wakeze na masuria zake wote, kwani alichukua wake 18 na masuria 60, akazaa wana wa kiume 28 na wa kike 60. Rehabeamu akamweka Abia, mwana wa Maka, kuwa mkuu na mwenye amri kwa ndugu zake, kwani alitaka kumpa ufalme. Kwa kuwa mwenye utambuzi akawatawanya wanawe wote katika nchi zote za Yuda na za Benyamini akiwaweka katika miji yote yenye maboma, akawapa vyakula vingi, akawaposea hata wanawake wengi. Ikawa, Rehabeamu alipokwisha kuushikiza ufalme wake na kuutia nguvu, akayaacha Maonyo ya Bwana, yeye na Waisiraeli wote pamoja naye. Katika mwaka wa tano wa mfalme Rehabeamu akapanda Sisaki, mfalme wa Misri, kuujia Yerusalemu, kwani waliyavunja maagano ya Bwana. Akaleta magari 1200 na wapanda farasi 60000 nao watu waliokuja naye toka Misri hawakuhesabika, Walibia na Wasuki na Wanubi. Akaiteka miji yenye maboma iliyokuwako Uyuda, akafika hata Yerusalemu. Ndipo, mfumbuaji Semaya alipokuja kwake mfalme Rehabeamu na kwa wakuu wa Wayuda waliokusanyika kwake Yerusalemu kwa ajili ya Sisaki, akawaambia: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana: Ninyi mmeniacha, basi, mimi nami nimewaacha na kuwatia mkononi mwa Sisaki. Ndipo, wakuu wa Isiraeli na mfalme walipojinyenyekeza, wakasema: Mwongofu ni Bwana! Bwana alipoona, ya kuwa wamejinyenyekeza, neno la Bwana likamjia Semaya kwamba: Kwa kuwa wamejinyenyekeza, sitawaangamiza, ila punde kidogo nitawapatia uponya, makali yangu yasimwagiwe Yerusalemu na huyo Sisaki. Lakini watakuwa watumishi wake, wapate kujua, utumishi wangu ulivyo, nao utumishi wa wafalme wa nchi nyingine ulivyo. Sisaki, mfalme wa Misri, akapanda, akaujia Yerusalemu, akavichukua vilimbiko vya Nyumbani mwa Bwana navyo vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme, vyote pia akavichukua, nazo ngao za dhahabu, Salomo alizozitengeneza, akazichukua. Mahali pao mfalme Rehabeamu akatengeneza ngao za shaba, akazitia mikononi mwa wakuu wa wapiga mbio waliongoja pa kuingia nyumbani mwa mfalme, waziangalie. Kila mara mfalme alipoingia Nyumbani mwa Bwana, hao walinzi wakaja, wakazichukua, kisha wakazirudisha chumbani mwao wapiga mbio. Kwa kuwa amejinyenyekeza, makali ya Bwana yakageuka na kumwacha, asimwangamize na kummaliza kabisa, maana katika nchi ya Yuda yalikuwamo bado mambo mema. Kisha mfalme Rehabeamu akapata nguvu tena mle Yerusalemu na kuushika ufalme. Alipoupata ufalme alikuwa mwenye miaka 41, akawa mfalme miaka 17 katika mji wa Yerusalemu, Bwana aliouchagua katika mashina yote ya Isiraeli, alikalishe Jina lake humo. Jina la mama yake ni Nama aliyekuwa Mwaamoni. Akayafanya yaliyokuwa mabaya, kwani hakuuelekeza moyo wake, umtafute Bwana. Mambo ya Rehabeamu, ya kwanza na ya mwisho, hayakuandikwa kwenye mambo ya mfumbuaji Semaya na ya mchunguzaji Ido, kama mambo ya wakale yalivyoandikwa? Lakini Rehabeamu na Yeroboamu walikuwa wakipigana vita siku zile zote. Kisha Rehabeamu akaja kulala na baba zake, akazikwa mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Abia akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa 18 wa mfalme Yeroboamu Abia akapata kuwa mfalme wa Wayuda. Akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 3; jina la mama yake ni Mikaya, binti urieli wa Gibeoni. Naye akapiga vita na Yeroboamu. Abia akajifunga kwenda vitani mwenye vikosi vya mafundi wa vita, watu 400000 waliochaguliwa. Naye Yeroboamu akajipanga vitani mwenye watu 800000 waliochaguliwa kwa kuwa mafundi wa vita wenye nguvu. Abia akaondoka kuja kusimama juu ya mlima wa Semaraimu ulioko milimani kwa Efuraimu, akasema: Nisikilizeni, Yeroboamu nanyi Waisiraeli wote! Je? Hamjui, ya kuwa Bwana Mungu wa Isiraeli alimpa Dawidi kuwa mfalme wa Waisiraeli kale na kale, yeye na wanawe, alipofanya naye agano la chumvi? Lakini Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyekuwa mtumishi wa Salomo, mwana wa Dawidi, akaondoka kwa kumkataa bwana wake na kuacha kumtii. Wakakusanyika kwake watu walio wa ovyoovyo tu wasiofaa kitu, wakajipatia nguvu za kumshinda Rehabeamu, mwana wa Salomo; kwani Rehabeamu alikuwa akingali kijana, nao moyo wake mchanga, hakuweza kujishupaza mbele yao. Sasa ninyi mnajiwazia, ya kuwa mtaweza kujishupaza mbele ya ufalme wa Bwana uliomo mikononi mwa wana wa Dawidi, kwa kuwa kwenu ni uvumi wa watu wengi, nazo ndama za dhahabu mnazo, Yeroboamu alizowatengenezea kuwa miungu yenu. Hamkuwafukuza watambikaji wa Bwana, wana wa Haroni, pamoja na Walawi, mkajifanyizia watambikaji, kama makabila ya nchi hizi? Kila ajaye na kuleta mtoto mume wa ng'ombe na madume saba ya kondoo, apate kulijaza gao lake, basi, hupata kuwa mtambikaji wao isiyo miungu. Lakini sisi Bwana Mungu wetu hakutuacha, nao wana wa Haroni wanamtumikia Bwana kuwa watambikaji, nao Walawi wanafanya kazi zao; kila kunapokucha na kila kunapokuchwa humvukizia Bwana wakimteketezea ng'ombe za tambiko na kumvikizia mavukizo yanukayo vizuri, tena humwekea mikate katika meza iliyo ya dhahabu tupu, tena hukiwasha kinara cha dhahabu na taa zake kila kunapokuchwa, kwani sisi tunaushika ulinzi wa Bwana Mungu wetu, lakini ninyi mmemwacha. Na mwone, ya kuwa Mungu yuko kwetu, ndiye anayetutangulia, nao watambikaji wake watapiga matarumbeta ya kuvumisha sana, wawazomee ninyi! Wana wa Isiraeli, msije kupigana na Mungu wa baba zenu! Kwani hamtafanikiwa. Lakini Yeroboamu alikuwa ametuma wengine, wawazunguke, wapate kuwavizia huko nyuma kuwajia migongoni kwao; kwa hiyo wengine wao walikuwa mbele ya Wayuda, nao waliowavizia walikuwa nyuma yao. Wayuda walipogeuka wakaona, ya kuwa hawana budi kupigana mbele na nyuma; ndipo, walipomlilia Bwana, watambikaji wakayapiga matarumbeta yao. Kisha watu wa Yuda wakapiga yowe; ikawa, watu wa Yuda walipopiga yowe, Mungu akampiga Yeroboamu na Waisiraeli wote mbele ya Abia na ya Wayuda. Ndipo, wana wa Isiraeli walipowakimbia Wayuda, naye Mungu akawatia mikononi mwao. Abia na watu wake wakawapiga, pigo likawa kubwa mno; kwao Waisiraeli wakaanguka kwa kuuawa watu 500000, nao ni watu wliochaguliwa. Ndivyo, wana wa Isiraeli walivyonyenyekezwa siku zile, lakini wana wa Yuda wakapata nguvu, kwa kuwa walimwegemea Bwana Mungu wa baba zao. Abia akakimbia, amfuate Yeroboamu na kumfukuza, akateka kwake miji, ndio Beteli na mitaa yake na Yesana na mitaa yake na Efuraimu na mitaa yake. Yeroboamu hakupata nguvu tena katika hizo siku za Abia, kisha Bwana akampiga, akafa. Abia akajipatia nguvu, akajichukulia wanawake 18, akazaa wana wa kiume 22 na wa kike 16. Mambo mengine ya Abia na njia zake na maneno yake yameandikwa katika kitabu cha maelezo ya mfumbuaji Ido. Abia akaja kulala na baba zake, wakamzika mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Asa akawa mfalme mahali pake. Siku zake nchi ikapata kutulia miaka kumi. Asa akayafanya mema yanyokayo machoni pake Bwana Mungu wake. Akapaondoa pa kutambikia miungu migeni na matambiko ya vilimani, akazivunja nazo nguzo za mawe za kutambikia, nayo miti ya Ashera akaikatakata. Akawaambia Wayuda, wamtafute Bwana Mungu wa baba zao, wayafanye Maonyo na maagizo yake. Katika miji yote ya Wayuda akayaondoa matambiko ya vilimani na mifano ya jua; kwa hivyo, alivyoushika ufalme, nchi ikatulia. Akajenga miji yenye maboma katika nchi ya Yuda, kwani nchi ilikuwa imetulia, hakuwa na vita vyo vyote katika miaka hiyo, kwani Bwana alimpatia utulivu. Kwa hiyo aliwaambia Wayuda: Na tuijenge miji hii na kuizungushia maboma na minara na kutia humo malango yenye makomeo; nchi hii ingaliko wazi mbele yetu, kwani tumemtafuta Bwana Mungu wetu; naye kwa hivyo, tulivyomtafuta, ametupatia kutulia pande zote. Basi, wakaijenga, wakafanikiwa. Asa akawa na vikosi vya watu walioshika ngao na mikuki, Wayuda 300000 na Wabenyamini walioshika ngao ndogo, waliojua hata kupinda pindi 280000; hawa wote walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu. Ndipo, alipotokea kwao Mnubi Zera mwenye vikosi vya watu milioni na magari 340, akaja mpaka Maresa. Asa akamtokea, wakajipanga kupigana katika bonde la Sefata karibu ya Maresa. Asa akamlalamikia Bwana Mungu wake akisema: Bwana, hakuna mwingine, usipokuwa wewe, anayeweza kumsaidia mwenye watu wengi naye asiye na nguvu; tusaidie, Bwana Mungu wetu! Kwani tumekuegemea wewe, tukaja kwa Jina lako kupigana na uvumi huu wa watu; Bwana, Mungu wetu ndiwe wewe! Hapa pasiwe na mtu atakayekushinda nguvu! Ndipo, Bwana alipowapiga Wanubi mbele ya Asa na mbele ya Wayuda, Wanubi wakakimbia. Asa akawakimbiza pamoja na hao watu, aliokuwa nao, mpaka Gerari; kwa Wanubi watu wakauawa kabisa, hakusalia kwao waliopona, kwani walivunjwa mbele ya Bwana na mbele ya vikosi vyake. Kisha Wayuda wakachukua mateka mengi sana. Wakaipiga miji yote pia iliyokuwa pande zote za Gerari, kwani tisho la Bwana lilikuwa limewaguia, wakazipokonya mali zote zilizokuwa katika miji hiyo yote, nazo mali za kupokonya zikawamo nyingi sana. Nayo mahema ya makundi wakayavunja, wakateka mbuzi na kondoo wengi, hata ngamia, kisha wakarudi Yerusalemu. Roho ya Mungu ikaja kumkalia Azaria, mwana wa Odedi, akamtokea Asa, akamwambia: Nisikilizeni, wewe Asa nanyi nyote Wayuda na Wabenyamini: Bwana yuko pamoja nanyi, mkiwa naye; mkimtafuta, atawaonekea ninyi, lakini mkimwacha, atawaacha nanyi. Siku nyingi Waisiraeli walikuwa pasipo Mungu wa kweli, pasipo mtambikaji aliyewafundisha Maonyo. Waliposongeka wakamrudia Bwana Mungu wa Isiraeli, wakamtafuta, naye akawaonekea. Siku zile hawakupata kutengemana, wala aliyetoka, wala aliyeingia, kwani wenyeji wote wa nchi hizi walikuwa na mahangaiko mengi. Ikasukumana, kabila na kabila nyingine, hata mji na mji mwingine, kwani Mungu aliwatisha na kuwasonga po pote. Lakini ninyi jitieni nguvu, wala msiilegeze mikono yenu! Kwani matendo yenu yatapata mshahara wao. Asa alipoyasikia hayo maneno ya ufumbuaji wa mfumbuaji Odedi akajishupaza, akayatowesha matapisho katika nchi yote ya Yuda na ya Benyamini, hata katika miji, aliyoiteka milimani kwa Efuraimu, nayo meza ya kumtambikia Bwana iliyokuwa mbele ya ukumbi wa Bwana akairudishia upya. Kisha akawakusanya Wayuda na Wabenyamini wote nao waliokaa ugenini kwake, Waefuraimu na Wamanase na Wasimeoni, kwani wengi waliokuwa Waisiraeli walirudi upande wake walipoona, ya kuwa Bwana Mungu wake yuko pamoja naye. Wakakusanyika Yerusalemu katika mwezi wa tatu wa mwaka wa kumi na tano wa Ufalme wa Asa, wakamtolea Bwana siku hiyo ng'ombe za tambiko, walizozitoa katika mateka: ng'ombe 700 na kondoo 7000. Wakaagana, wamtafute Bwana Mungu wa baba zao kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kwamba: Kila asiyemtafuta Bwana Mungu wa Isiraeli auawe, mdogo kwa mkubwa, mume kwa mke. Wakamwapia Bwana kuyafanya hayo wakipaza sauti za kumshangilia na kupiga matarumbeta na mabaragumu. Wayuda wote wakakifurahia hicho kiapo, kwani waliapa kwa mioyo yao yote; kwa kuwa walimtafuta Bwana kwa kupendezwa kabisa, akawaonekea, akawapatia kutulia pande zote. Mfalme Asa akamwondoa naye mama yake Maka katika ukuu wake, kwa kuwa alitengeneza kinyago cha Ashera, nacho kinyago chake Asa akakikatakata na kukipondaponda, kisha akakiteketeza penye kijito cha Kidoroni. Lakini matambiko ya vilimani hayakutoweka kwao Waisiraeli, lakini moyo wake Asa ulikuwa mtimilifu siku zake zote. Navyo, baba yake alivyovitakasa, pamoja navyo alivyovitakasa mwenyewe, fedha na dhahabu na vyombo, akavipeleka Nyumbani mwa Mungu. Vita havikuwako hata mwaka wa 35 wa ufalme wa Asa. Katika mwaka wa 36 wa ufalme wa Asa ndipo, Basa, mfalme wa Waisiraeli, alipopanda kuijia nchi ya Yuda, akajenga Rama, asipatikane mtu anayeweza kutoka wala kuingia kwa Asa, mfalme wa Wayuda. Ndipo, Asa alipochukua fedha na dhahabu katika vilimbiko vya Nyumba ya Bwana na vya nyumba ya mfalme, akazituma kwake Benihadadi, mfalme wa Ushami, aliyekaa Damasko, kumwambia: Liko agano, tuliloliagana mimi na wewe, naye baba yangu na baba yako; kwa hiyo ninatuma kwako fedha na dhahabu. Nenda, ulivunje agano, uliloliagana na Basa, mfalme wa Waisiraeli, aondoke kwangu! Benihadadi akamwitikia mfalme Asa, akawatuma wakuu wa vikosi vyake, alivyokuwa navyo, kwenda kupigana na miji ya Waisiraeli, wakaiingia miji ya Iyoni na Dani na Abeli-Maimu na miji yote ya Nafutali iliyokuwa yenye vilimbiko. Basa alipoyasikia haya akaacha kuujenga Rama na kuzikomesha kazi zake. Kisha mfalme Asa akawatwaa Wayuda wote, wakayachukua mawe ya huko Rama nayo miti yake, Basa aliyoitumia ya kujenga Rama, naye akaitumia ya kujenga Geba na Misipa. Siku hizo mtazamaji Hanani akaja kwa Asa, mfalme wa Wayuda, akamwambia: Kwa kuwa umemwegemea mfalme wa Ushami, usimwegemee Bwana Mungu wako, kwa hiyo vikosi vya mfalme wa Ushami vimeponyoka mkononi mwako. Wale Wanubi na Walibia hawakuwa vikosi vingi vyenye magari na wapanda farasi wengi mno? Lakini kwa kuwa ulimwegemea Bwana, akawatia mkononi mwako. Kwani macho ya Bwana huzunguka katika nchi zote, ajitokeze kuwa mwenye nguvu kwao waliomwelekezea mioyo yao yote mizima. Katika jambo hili umefanya upumbavu, kwa hiyo tangu sasa huna budi kupiga vita. Asa akamkasirikia mtazamaji, akamfunga nyumbani mwenye mikatale, kwani alimchafukia kwa ajili ya hayo. Nao watu wengine Asa akawakorofisha siku zile. Mambo ya Asa, ya kwanza na ya mwisho, tukitaka kuyatazama, tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Wayuda na wa Waisiraeli. Katika mwaka wa 39 wa ufalme wake Asa akaugua miguu, huu ugonjwa wake ukazidi sana; namo katika huu ugonjwa wake hakumtafuta Bwana, ila waganga. Kisha Asa akaja kulala na baba zake, akafa katika mwaka wa 41 wa ufalme wake. Wakamzika penye makaburi yake, aliyojichimbia mjini mwa Dawidi; wakamlaza katika kilalo walichokijaza uvumba wa namna nyingi na manukato yaliyotengenezwa na mafundi, wakamvukizia mavukizo makubwa sana. Mwanawe Yosafati akawa mfalme mahali pake, akajipatia nguvu za kuwatawala Waisiraeli. Akaweka vikosi vya askari katika miji yote ya Yuda iliyokuwa na maboma, kisha akaweka wenye amri katika nchi ya Yuda, namo katika miji ya Efuraimu, baba yake Asa aliyoiteka. Bwana akawa naye Yosafati, kwani aliendelea katika njia ya kwanza ya babu yake Dawidi, asiitafute miungu ya Baali, ila alimtafuta Mungu wa baba yake, akaendelea na kuyashika maagizo yake, asifanye matendo ya Waisiraeli. Kwa hiyo Bwana akaushupaza ufalme wake mkononi mwake, Wayuda wote wakampa Yosafati matunzo, akapata mali na macheo mengi. Kwa kuzishika njia za Bwana moyo wake ukawa mkuu, kisha akayaondoa matambiko ya vilimani na miti ya Ashera katika nchi ya Yuda. Katika mwaka wa tatu wa ufalme wake akatuma watu wake Benihaili na Obadia na Zakaria na Netaneli na Mikaya, waende kufundisha watu katika miji ya Yuda; pamoja nao walikuwa Walawi Semaya na Netania na Zebadia na Asaheli na Semiramoti na Yonatani na Adonia na Tobia na Tobu-Adonia; pamoja nao hawa Walawi walikuwa watambikaji Elisama na Yoramu. Wakawafundisha watu katika nchi ya Yuda wakikishika kitabu cha Maonyo ya Bwana, wakazunguka katika miji yote ya Yuda na kufundisha watu. Stusho la Bwana likaziguia nchi zote zenye wafalme zilizoizunguka nchi ya Yuda, wasipigane na Yosafati. Kwao Wafilisti wakatoka wajumbe, wakamletea Yosafati matunzo na fedha, walizozichanga, Waarabu nao wakamletea mbuzi na kondoo, madume ya kondoo walikuwa 7700, hata madume ya mbuzi 7700. Ndivyo, Yosafati alivyoendelea kuwa mkuu zaidi, akajenga katika nchi ya Yuda ngome na miji yenye vilimbiko. Akawa na mapato mengi mle mijini mwa Yuda, namo Yerusalemu akawa na watu wa kupiga vita waliokuwa mafundi wenye nguvu. Wakijipanga kwa milango ya baba zao, ikawa hivyo: Wayuda walikuwa na wakuu wa maelfu, mkuu mwenyewe ni Adina, pamoja naye wakawa mafundi wa vita wenye nguvu 300000. Wa pili ni mkuu Yohana, pamoja naye wakawa watu 280000. Akafuatwa na Amasia, mwana wa Zikiri, aliyejitoa mwenyewe kuwa mtu wa Bwana, pamoja naye wakawa mafundi wa vita wenye nguvu 200000. Kwao Wabenyamini Eliada alikuwa fundi wa vita mwenye nguvu, pamoja naye wakawa watu 200000 waliochukua pindi na ngao. Wa pili alikuwa Yozabadi, pamoja naye wakawa watu 180000 wenye mata ya vita. Hawa ndio waliomtumikia mfalme kuliko wale, mfalme aliowaweka katika miji yenye maboma katika nchi yote ya Yuda. Ikawa, Yosafati alipopata mali na macheo mengi akamwoza mwanawe binti Ahabu. Miaka ilipopita michache, akashuka kwenda Samaria kwake Ahabu; Ahabu akamchinjia yeye na watu wake, aliokuwa naye, mbuzi na kondoo na ng'ombe wengi, akamchochea kupanda Ramoti wa Gileadi. Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, akamwuliza Yosafati, mfalme wa Wayuda: Utakwenda pamoja na mimi Ramoti wa Gileadi? Akamwambia: Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, tutakwenda pamoja na wewe vitani. Kisha Yosafati akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Uliza leo hivi, Bwana atakavyosema! Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipowakusanya wafumbuaji, watu 400, akawauliza: Twende Ramoti wa Gileadi kupga vita au niache? Wakasema: Panda tu! Mungu atautia mkononi mwa mfalme. Yosafati akauliza: Huku hakuna tena mfumbuaji wa Bwana, tumwulize naye? Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: Yuko bado mtu mmoja wa kumwuliza neno la Bwana, lakini mimi ninamchukia, kwani hanifumbulii yatakayokuwa mema, ila siku zote husema yatakayokuwa mabaya, naye ndiye Mikaya, mwana wa Imula. Yosafati akasema: Mfalme asiseme hivyo! Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipomwita mtumishi mmoja wa nyumbani, akamwambia: Piga mbio kumwita Mikaya, mwana wa Imula! Mfalme wa Waisiraeli na Yosafati, mfalme wa Wayuda, walikuwa wamekaa kila mmoja katika kiti chake cha kifalme na kuvaa mavazi, wakawa wakikaa hapo pa kupuria ngano penye lango la kuuingilia mji wa Samaria, nao wafumbuaji wote wakawa wakifumbua mbele yao. Ndipo, Sedekia, mwana wa Kenaana, alipojifanyizia pembe za chuma, akasema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa pembe kama hizi utawakumba Washami, mpaka uwamalize. Nao wafumbuaji wote wakafumbua hivyo kwamba: Upandie Ramoti wa Gileadi! Utafanikiwa, naye Bwana atautia mkononi mwake mfalme. Yule mjumbe aliyekwenda kumwita Mikaya akamwambia kwamba: Tazama, maneno ya wafumbuaji ni kinywa kimoja tu cha kufumbua mema yatakayomjia mfalme, Basi, neno lako nalo na liwe kama neno la mmoja wao hao, useme mema yatakayokuwa. Mikaya akasema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, nitasema hayo tu, Mungu wangu atakayoniambia. Alipofika kwake mfalme, mfalme akamwuliza: Mika, twende Ramoti wa Gileadi kupiga vita au niache? Akasema: Pandeni! Mtafanikiwa, maana watatiwa mikononi mwenu. Mfalme akamwambia: Nimekuapisha mara nyingi, usiniambie mengine katika Jina la Bwana, isipokuwa iliyo ya kweli. Ndipo, aliposema: Nimewaona Waisiraeli, nao walikuwa wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Bwana akasema: Hawa hawana bwana, na warudi na kutengemana kila mtu nyumbani kwake. Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: Sikukuambia: Hanifumbulii yatakayokuwa mema, ila yatakayokuwa mabaya tu? Mikaya akasema: Lakini lisikieni neno la Bwana! Nimemwona Bwana, akikaa katika kiti chake kitukufu, navyo vikosi vyote vya mbinguni vikasimama kuumeni na kushotoni kwake. Bwana akauliza: Yuko nani atakayemponza Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, aje kuupandia Ramoti wa Gileadi, aangushwe huko? Wakajibu, mmoja akisema hivi, mmoja hivi. Kisha akatokea roho, akasimama mbele ya Bwana, akasema: Mimi nitamponza. Bwana akamwuliza: Kwa nini? Akasema: Nitatoka kuwa roho ya uwongo vinywani mwa wafumbuaji wake wote. Bwana akasema: Utamponza kweli, utaweza hivyo, toka kufanya hivyo! Sasa tazama! Bwana ametia roho ya uwongo vinywani mwa hawa wafumbuaji wako, maana yeye Bwana amekwisha kukutakia mabaya. Ndipo, Sedekia, mwana wa Kenaana, alipomkaribia Mikaya, akampiga makofi na kumwuliza: Roho ya Mungu imeshika njia gani, inipite mimi, ije kusema na wewe? Mikaya akasema: Jiangalie! Utaviona siku hiyo, utakapoingia chumba kwa chumba, upate kujificha. Mfalme wa Waisiraeli akasema: Mchukueni Mikaya, mmrudishe kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoasi, mwana wa mfalme, mseme: Hivi ndivyo, mfalme anavyosema: Mwekeni huyu kifungoni, mmpe chakula cha mahangaiko na maji ya mahangaiko, hata nitakaporudi salama. Mikaya akasema: kama utarudi salama, Bwana hakusema kinywani mwangu. Kisha akasema: Lisikieni hili, ninyi makabila yote! Kisha mfalme wa Waisiraeli na Yosafati, mfalme wa Wayuda, wakapanda kwenda Ramoti wa Gileadi. Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: nitavaa nguo nyingine, niingie penye mapigano, lakini wewe zivae nguo zako! Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipovaa nguo nyingine, kisha wakafika penye mapigano. Naye mfalme wa Ushami alikuwa amewaagiza wakuu wa magari, aliokuwa nao, kwamba: Msipigane na mtu ye yote, mdogo kwa mkubwa, ila mpigane na mfalme wa Waisiraeli peke yake tu! Ikawa, wakuu wa magari walipomwona Yosafati wakamwazia yeye kuwa mfalme wa Waisiraeli, wakamzunguka kupigana naye. Ndipo, Yosafati alipopiga yowe, Bwana akamsaidia, yeye Mungu akawaondoa hapo, alipokuwa, na kuwadanganyadanganya. Ikawa, wakuu wa magari walipoona, ya kuwa siye mfalme wa Waisiraeli, wakarudi na kuacha kumfuata. Kulikuwa na mtu, akauvuta upindi wake kwa kubahatisha tu, akampiga mfalme wa Waisiraeli hapo, vyuma vya kisibau chake vilipounganishwa. Ndipo, alipomwambia mwendeshaji wa gari: ligeuze kwa mkono wako, unitoe hapa, wanapopigana, kwani nimeumia. Mapigano yakazidi siku hiyo, kwa sababu hii mfalme wa Waisiraeli alikuwa amejisimamisha garini ng'ambo ya huku kuwaelekea Washami hata jioni, akafa, jua lilipokuchwa. Yosafati, mfalme wa Wayuda, aliporudi nyumbani kwake kutengemania Yerusalemu, Yehu, mwana wa Hanani, aliyekuwa mchunguzaji akamtokea, akamwambia mfalme Yosafati: Inakuwaje, ukipenda kumsaidia asiyemcha Mungu, nao wanaomchukia Bwana? Kwa sababu hii makali yatokayo kwake Bwana yanakukalia. Lakini tena yako mema yaliyoonekana kwako, kwani umevitowesha vinyago vya Ashera katika nchi hii, ukauelekeza moyo wako kumtafuta Mungu. Yosafati alipokaa Yerusalemu kidogo, akatoka tena kwenda kwa watu, akawaanzia wa Beri-Seba, hata awafikie wa milimani kwa Efuraimu, akawarudisha kwake Bwana Mungu wa baba zao. Akaweka waamuzi katika nchi hii katika miji yote ya Yuda iliyokuwa yenye maboma, mji kwa mji, akawaambia waamuzi: yaangalieni mtakayoyafanya! Kwani sio watu, mnaowafanyia kazi ya uamuzi, ila Bwana, naye yuko pamoja nanyi, mnapokata mashauri. Kwa sababu hii tisho la Bwana na liwakalie, mzifanye kazi zenu na kujiangalia! Kwani kwake Bwana hakuna wala upotovu, wala upendeleo, wala upenyezi. Namo Yerusalemu Yosafati akaweka Walawi wengine na watambikaji, hata wakuu wengine wa milango ya Isiraeli kumfanyizia Bwana kazi ya uamuzi na kuwagombea watu. Waliporudi Yerusalemu, akawaagiza kwamba: Haya myafanye kwa kumwogopa Bwana na kwa welekevu na kwa mioyo yote! Katika magomvi yote yatakayoletwa kwenu na ndugu zenu wanaokaa katika miji yao, kama ni kugombeana damu zilizomwagwa au maonyo na maagizo au maongozi na maamuzi, mtawafundisha, wasimkosee Bwana, makali yakawajia ninyi nao walio ndugu zenu. Fanyeni hivyo, msikore manza! Tazameni, mtambikaji mkuu Amaria atawaongoza katika mambo yote ya Bwana, naye Zebadia, mwana wa Isimaeli, mwenye amri wa mlango wa Yuda, atawaongoza katika mambo yote ya mfalme, nao Walawi wako mbele yenu kuwasimamia watu. Jipeni mioyo, kafanyeni hivyo! Ndipo, Bwana atakapokuwa nao wale walio wema. Ikawa baada ya hayo, wakaja wana wa Moabu na wana wa Amoni pamoja na Waamoni wengine kumpelekea Yosafati vita. Watu wakaja kumpasha Yosafati habari kwamba: Uvumi wa watu wengi unakujia, unatoka ng'ambo ya huko ya bahari upande wa Ushami, nao wamekwisha kufika Hasesoni-Tamari, ndio Engedi. Yosafati akaogopa, akamwelekezea Bwana uso wake na kulitafuta shauri lake, akatangaza katika nchi yote ya Yuda, watu wafunge. Wayuda wakakusanyika kutafuta msaada kwa Bwana; walipokwisha kufika na kutoka katika miji yote ya Yuda, wamtafute Bwana, Yosafati akaja kusimama katika huo mkutano wa Wayuda na Wayerusalemu Nyumbani mwa Bwana mbele ya ua mpya, akasema: Bwana Mungu wa baba zetu, wewe siwe Mungu akaaye mbinguni na kuzitawala nchi zote za wamizimu zenye wafalme? Mkononi mwako zimo nguvu na uwezo mwingi, hakuna awezaye kujisimamisha kwako. Wewe hukuwafukuza wenyeji wa nchi hii mbele yao walio ukoo wako wa Waisiraeli, ukaitoa na kuwapa wao wa uzao wa mpenzi wako Aburahamu, iwe yao kale na kale? Wakakaa huku, wakakujengea huku Patakatifu pa Jina lako kwa kwamba: Mabaya yatakapotujia, kama panga za kutupatiliza au magonjwa ya kuambukiza au njaa, tuje kusimama mbele ya Nyumba hii na kukulalamikia usoni pako kwa kusongeka kwetu, kwani Jina lako linakaa humu Nyumbani; ndipo, utakapotusikia, utuokoe. Sasa watazame hawa wana wa Amoni na wa Moabu na wa milima ya Seiri! Hapo, Waisiraeli walipotoka katika nchi ya Misri, hukuwapa ruhusa kuingia kwao hawa; kwa hiyo waliondoka kwao pasipo kuwaangamiza. Sasa unawaona, wanavyotufanyizia wakija kutufukuza katika nchi hii, uliyotupatia, utupe sisi, iwe fungu letu. Mungu wetu, hutaki kuwapatiliza? Kwani kwetu sisi hakuna nguvu za kuushinda huu uvumi ya watu wengi mno waliotujia. Sisi hatujui la kufanya, kwa hiyo macho yetu yanakuelekea. Nao Wayuda wote walikuwa wamesimama mbele ya Bwana pamoja na watoto wao wachanga na wanawake na wana wao. Ndipo, Yahazieli, mwana wa Zakaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yieli, mwana wa Matania, aliyekuwa Mlawi wa mlango wa Asafu, alipoingiwa na Roho ya Bwana pale katikati ya mkutano, akasema: Ninyi Wayuda wote nanyi wenyeji wa Yerusalemu na wewe mfalme Yosafati, sikilizeni: Haya ndiyo, Bwana anayowaambia: Msiogope, wala msiingiwe na vituko mkiuona uvumi huu wa watu wengi! Kwani vita hivi si vyenu, ila vya Mungu. Kesho shukeni kwenda kwao! Ndipo, mtakapowaona, wakipanda pa kupandia kwenda Sisi, nanyi mtawakuta kwenye mwisho wa bonde lililoko mbele ya nyika ya Yerueli. Lakini ninyi hamtapigana huko, jipangeni tu na kusimama, mwone, Bwana atakavyowapatia wokovu, ninyi Wayuda na Wayerusalemu! Msiogope, wala msiingiwe na vituko! Kesho watokeeni tu! Naye Bwana atakuwa nanyi. Ndipo, Yosafati alipouinamisha uso wake hata chini, hata Wayuda wote pamoja na wenyeji wa Yerusalemu wakamwangukia Bwana na kumwomba. Kisha wakainuka Walawi waliokuwa wa mlango wa Kehati na wa Kora kumshangilia Bwana Mungu wa Isiraeli, wakizipaza kabisa sauti zao ziwe kuu. Kesho yake wakaondoka na mapema kwenda nyikani kwa Tekoa; hapo, walipotoka, Yosafati akasimama hapo akisema: Nisikilizeni, ninyi Wayuda na wenyeji wa Yerusalemu! Mtegemeeni Bwana Mungu wenu, ndipo, mtakaposhupazwa! Wategemeeni nao wafumbuaji wake, ndipo, mtakapofanikiwa! Alipokwisha kuwapa watu shauri hili akaweka watakaomwimbia Bwana nao watakaoutukuza urembo wa Patakatifu, watoke na kuwatangulia wenye mata na kusema: Mshukuruni Bwana, ya kuwa upole wake ni wa kale na kale! Papo hapo, walipoanza kupiga yowe na shangwe, ndipo, Bwana alipoleta watu wa kuwavizia wana wa Amoni na wa Moabu nao wa milima ya Seiri walioingia katika nchi ya Yuda. Maana wana wa Amoni na wa Moabu wakawainukia wenyeji wa milimani kwa Seiri na kuwaua na kuwaangamiza, walipokwisha kuwamaliza wenyeji wa Seiri, wakasaidiana kila mtu na mwenzake kuuana. Wayuda walipofika hapo pa kuchungulia nyikani, wakiugeukia ule uvumi wa watu, wakaona mizoga tu iliyolala chini, hakuwako aliyepona. Ndipo, Yosafati na watu wake walipokuja kujichukulia nyara, wakaona kwao mali nyingi penye hiyo mizoga na vyombo vyenye kima, wakawavua vingi mno, wasiweze kuvichikua vyote; wakawako siku tatu wakipokonya nyara, kwani zilikuwa nyingi. Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Tukuzo, kwani huko ndiko, walikomtukuzia Bwana; kwa sababu hii mahali pale wakapaita Bonde la Tukuzo hata leo. Kisha watu wote wa Yuda na wa Yerusalemu wakarudi, naye Yosafati akawatangulia kurudi Yerusalemu na kufurahi, kwani Bwana aliwapa kuwafurahia adui zao. Wakaingia Yerusalemu na kupiga mapango na mazeze na matarumbeta, wakaingia Nyumbani mwa Bwana. Tisho la Bwana likaziguia hizo nchi zote zenye wafalme, waliposikia, ya kama Bwana amepigana na adui za Waisiraeli. Kwa hiyo ufalme wa Yosafati ukapata kutengemana, Mungu wake akimpatia utulivu pande zote. Yosafati akawa mfalme wa Wayuda, naye alikuwa mwenye miaka 35 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 25. Jina la mama yake ni Azuba, binti Silihi. Akaendelea kuishika njia ya baba yake Asa, hakuiacha kabisa, akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana. Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, kwani watu hawajamwelekezea Mungu wa baba zao mioyo yao. Mambo mengine ya Yosafati, ya kwanza na ya mwisho, tunayaona, yameandikwa katika mambo ya Yehu, mwana wa Hanani, yaliyotiwa katika kitabu cha wafalme wa Waisiraeli. Baada ya hayo Yosafati, mfalme wa Wayuda, akajiunga na Ahazia, mfalme wa Waisiraeli; lakini huyu matendo yake, aliyoyafanya, yalikuwa maovu. Akajiunga naye kwa kutengeneza merikebu za kwenda Tarsisi; wakatengeneza merikebu hata huko Esioni-Geberi. Eliezeri, mwana wa Dodawa wa Maresa, akamfumbulia Yosafati kwamba: Kwa kuwa umejiunga na Ahazia, Bwana atazivunja hizi kazi zako. Kwa hiyo vyombo vikavunjika, havikuweza kwenda Tarsisi. Yosafati akaja kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa Dawidi. Naye mwanawe Yoramu akawa mfalme mahali pake. Yoramu alikuwa na ndugu, nao walikuwa wana wa Yosafati, ndio Azaria na Yehieli na Zakaria na Azaria na Mikaeli na Sefatia; hawa wote walikuwa wana wa Yosafati, mfalme wa Waisiraeli. Hawa baba yao aliwapa vipaji vingi vya fedha na vya dhahabu na vya vitu vyenye kima, pamoja na miji yenye maboma katika nchi ya Yuda, lakini ufalme alimpa Yoramu, kwani huyu alikuwa mwanawe kwa kwanza. Yoramu alipokwisha kujisimikia ufalme wa baba yake na kujipatia nguvu, akawaua ndugu zake wote kwa upanga, hata wakuu wengine wa Waisiraeli Yoramu alikuwa mwenye miaka 32 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 8. Akaendelea katika njia za wafalme wa Waisiraeli, kama wale wa mlango wa Ahabu walivyofanya, kwani binti Ahabu alikuwa mkewe; basi, naye akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana. Lakini Bwana hakutaka kuuangamiza mlango wa Dawidi kwa ajili ya agano, alilolifanya na Dawidi, kwa kuwa alisema, ya kama atampa yeye na wanawe kuwa taa iwakayo siku zote. Katika hizo siku zake Waedomu wakalivunja agano wakijitoa mikononi mwa Wayuda, wakajiwekea mfalme wa kuwatawala. Ndipo, Yoramu alipoondoka kuwaendea pamoja na wakuu wake, akiyachukua magari yote. Ikawa, alipoondoka usiku, akawapiga Waedomu waliomzunguka yeye na wakuu wa magari. Lakini Waedomu wakalivunja agano tena, wakajitoa mikononi mwa Wayuda mpaka siku hii ya leo. Siku zile ndipo, nao wa Libuna walipolivunja agano na kujitoa mkononi mwake, kwani alimwacha Bwana Mungu wa baba zake. Yeye naye akafanya matambiko ya vilimani katika milima ya Yuda; ndivyo, alivyowazinisha wenyeji wa Yerusalemu, nao Wayuda akawaponza. Ikafika kwake barua ya mfumbuaji Elia ya kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa baba yako Dawidi anavyosema: kwa kuwa hukuendelea katika njia za baba yako Yosafati, wala katika njia za Asa, mfalme wa Wayuda, ukaendelea katika njia za wafalme wa Waisiraeli, ukawazinisha Wayuda na wenyeji wa Yerusalemu, kama mlango wa Ahabu ulivyozini, ukawaua nao ndugu zako wa mlango wa baba yako waliokuwa wema kuliko wewe, na umwone Bwana, akiwapiga pigo kubwa watu wako, hata wanao na wake zako na mali zako zote. Lakini wewe utapatwa na magonjwa mengi kwa kuugua tumboni mwako, mpaka matumbo yako yatokee kwa kuugua hivyo siku nyingi na nyingi. Kisha Bwana akaziamsha roho za Wafilisti na za Waarabu waliopakana na Wanubi, wamjie Yoramu. Wakapanda katika nchi ya Yuda na kujipenyeza huko, wakaziteka mali zote zilizoonekana nyumbani mwa mfalme, hata watoto wake na wakeze, hakusalia mtoto kwake ila Yoahazi tu aliyekuwa mdogo katika wanawe wote. Baada ya hayo Bwana akampiga tumboni mwake, apate ugonjwa usio na mganga wa kuuponya. Ukawa wa siku nyingi na nyingi; matumbo yake yakatokea kwa huo ugonjwa, siku zilipokwisha kupita kama miaka miwili, akafa na kuumia vibaya. Kisha watu wake hawakumteketezea manukato, kama walivyowateketezea baba zake. Alikuwa mwenye miaka 32 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 8, akajiendea pasipo kuombolezewa, wakamzika mjini mwa Dawidi, lakini hawakumzika makaburini kwa wafalme. Wenyeji wa Yerusalemu wakampa mwanawe mdogo Ahazia ufalme mahali pake, kwani wakubwa wake wote waliuawa na kikosi kilichokuja na Waarabu kambini. Ndivyo, Ahazia, mwana wa Yoramu, alivyopata kuwa mfalme wa Wayuda. Alikuwa mwenye miaka 22, alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu mwaka mmoja. Jina la mama yake ni Atalia, binti Omuri. Yeye naye akaendelea katika njia za mlango wa Ahabu, kwani mama yake ndiye aliyemwongoza kuyafanya yaliyo maovu. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kama mlango wa Ahabu, kwani hao ndio waliomwongoza, baba yake alipokwisha kufa, wampatie mwangamizo. Kwa kuongozwa nao akaja kwenda na Yoramu, mwana wa Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, kumpelekea Hazaeli, mfalme wa Ushami, vita huko Ramoti wa Gileadi. Washami walipomwumiza Yoramu, akarudi Izireeli, apate watakao mponya vidonda, walivyompiga kule Rama, alipopigana na Hazaeli, mfalme wa Ushami. Ndipo, Azaria, mwana wa Yoramu, mfalme wa Wayuda, aliposhuka kumtazama Yoramu, mwana wa Ahabu, huko Izireeli, kwani ndiko, alikougulia. Hili lilitoka kwake Mungu kuwa mwangamizo wake Ahazia, alipofika kwa Yoramu: kwani alipokwisha kufika akatoka pamoja na Yoramu kwenda kupigana na Yehu, mwana wa Nimusi, Bwana aliyempaka mafuta, aung'oe mlango wa Ahabu. Ikawa, Yehu alipoupatiliza mlango wa Ahabu, akawaona nao wakuu wa Wayuda na wana wa ndugu zake Ahazia waliomtumikia Ahazia, akawaua. Alipoagiza kumtafuta Ahazia, wakamkamatia Samaria, alikojificha, wakampeleka kwa Yehu, wakamwua, wakamzika, kwani walisema: Yeye ni mwana wa Yosafati aliyemtafuta Bwana kwa moyo wake wote. Lakini katika mlango wa Ahazia hakuwako mwenye nguvu aliyeweza kuwa mfalme. Atalia, mamake Ahazia, alipoona, ya kuwa mwanawe amekufa, akaondoka, akawaua wazao wote wa kifalme wa mlango wa Yuda. Lakini Yosabati, binti mfalme, akamchukua Yoasi, mwana wa Ahazia, akamwiba katikati ya wana wa mfalme waliokwenda kuuawa, akamweka pamoja na mnyonyeshaji wake katika chumba cha kulalia. Ndivyo, Yosabati, binti mfalme Yoramu, mkewe mtambikaji Yoyada, aliyekuwa umbu lake Ahazia, alivyomficha Yoasi, Atalia asimwone, asipate kumwua. Akakaa kwao Nyumbani mwa Mungu na kufichwa miaka sita, Atalia alipokuwa mfalme wa kike wa nchi hiyo. Katika mwaka wa saba Yoyada akajishupaza, akawachukua wakuu wa mamia, Azaria, mwana wa Yerohamu, na Isimaeli, mwana wa Yohana, na Azaria, mwana wa Obedi, na Masea, mwana wa Adaya, na Elisafati, mwana wa Zikiri, akafanya maagano nao. Wakazunguka katika nchi ya Yuda, wakawakusanya Walawi na kuwatoa katika miji yote ya Yuda pamoja na wakuu wa milango ya Isiraeli, wakaja Yerusalemu. Huu mkutano wote ukafanya agano na mfalme Nyumbani mwa Mungu, Yoyada akawaambia: Mtazameni huyu mwana wa mfalme! Atakuwa mfalme, kama Bwana alivyosema kwa ajili ya wana wa Dawidi. Hili ndilo neno, mtakalolifanya: fungu lenu la tatu, ninyi watambikaji na Walawi, watakaoingia kazi siku ya mapumziko, sharti walinde malangoni; fungu jingine la tatu sharti walinde nyumbani mwa mfalme, fungu jingine la tatu walinde langoni penye msingi. Kisha watu wote waje nyuani penye Nyumba ya Bwana. Lakini Nyumbani mwa Bwana mtu asiingie, wasipokuwa watambikaji nao Walawi wanaotumikia. Hao wataingia, kwani ndio watakatifu. Nao watu wote sharti walinde ulinzi wa Bwana, nao Walawi sharti wamzunguke mfalme pande zote, kila mtu akiyashika mata yake, kisha kila atakayeingia Nyumbani mwa Bwana na auawe! Hivyo sharti mwe na mfalme, akiingia, hata akitoka. Walawi na Wayuda wote wakayafanya yote, kama mtambikaji Yoyada alivyowaagiza, kila mtu akawachukua wate wake walioingia kazi siku ya mapumziko nao waliotoka kazi siku ya mapumziko, kwani mtambikaji Yoyada hakuwapa ruhusa waliozimaliza zamu. Kisha mtambikaji Yoyada akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao ndogo na kubwa za mfalme Dawidi zilizokuwa Nyumbani mwa Mungu. Akawapanga watu wote, kila mtu na mkuki wake mkononi mwake kuanzia upande wa kuume wa Nyumba kuufikia upande wa kushoto wa Nyumba, kuifikia meza ya kutambikia na tena kuifikia Nyumba yenyewe, wamzunguke mfalme pande zote. Kisha wakamtoa mwana wa mfalme, wakamvika kilemba cha kifalme, wakampa nacho kizingo cha Ushahidi, wakamfanya kuwa mfalme, Yoyada na wanawe wakimpaka mafuta na kusema: pongezi, mfalme! Atalia alipozisikia sauti za watu waliomkimbilia mfalme na kumshangilia, akaja naye hapo, watu walipo, penye Nyumba ya Bwana. Alipotazama, akamwona mfalme, akisimama katika ulingo wake pa kuingilia, nao wakuu na wapiga matarumbeta wakisimama kwake mfalme, nao watu wote wa nchi yao wakawa wenye furaha na kupiga matarumbeta, nao waimbaji wakavipiga vyombo vya kuimbia, wakawaongoza watu kushangilia. Ndipo, Atalia alipoyararua mavazi yake na kupiga kelele kwamba: Mmedanganyika! Mmedanganyika! Ndipo, mtambikaji Yoyada alipowatoa wakuu wa mamia waliovisimamia vikosi, akawaambia: Mtoeni hapa penye mipango ya watu! Naye atakayemfuata na auawe kwa upanga! Kwani mtambikaji alisema: Msimwue Nyumbani mwa Bwana! Wakamkamata kwa mikono, naye alipofika pa kuliingilia lango la farasi penye nyumba ya mfalme, wakamwua huko. Kisha Yoyada akafanya agano, yeye na watu wote na mfalme, wawe ukoo wake Bwana. Ndipo, watu wote walipoiingia nyumba ya Baali, wakaibomoa; nazo meza za kumtambikia na vinyago vyake wakavivunjavunja kabisa, naye Matani, mtambikaji wa Baali, wakamwua mbele ya meza za kutambikia. Kisha Yoyada akaweka watambikaji na Walawi kuwa wakaguzi wa Nyumba ya Bwana, kwani Dawidi aliwapatia hao kazi ya kuiangalia Nyumba ya Bwana, wamteketezee Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, kama ilivyoandikwa katika Maonyo ya Mose, pamoja na kuimba nyimbo za furaha, kama Dawidi alivyowaongoza. Akaweka nao walinda malango ya Nyumba ya Bwana, mtu asiingie akiwa mwenye uchafu kwa jambo lo lote. Kisha akawachukua wakuu wa mamia na watukufu na watawalaji wa watu nao watu wote wa nchi hii, akamtoa mfalme Nyumbani mwa Bwana, wakaingia nyumbani mwa mfalme na kupita katikati katika lango la juu, wakamketisha mfalme katika kiti cha kifalme. Wakafurahi watu wote wa nchi hii, nao mji ukatulia. Lakini Atalia walikuwa wamemwua kwa upanga. Yoasi alikuwa mwenye miaka 7 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 40. Jina la mama yake ni Sibia wa Beri-Seba. Yoasi akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana siku zote, mtambikaji Yoyada alizokuwapo. Yoyada akamwoza wake wawili, akazaa wana wa kiume na wa kike. Ikawa baada ya hayo, Yoasi akajipa moyo wa kuirudishia Nyumba ya Bwana upya. Akawakusanya watambikaji na Walawi, akawaambia: Tokeni, mwende katika miji yote ya Yuda, mkusanye kwa Waisiraeli wote fedha za kuitengeneza Nyumba ya Mungu wenu mwaka kwa mwaka! Neno hili na mlifanye kwa upesi! Lakini Walawi hawakulifanya kwa upesi. Ndipo, mfalme alipomwita Yoyada aliyekuwa mkuu wao, akamwambia: Mbona hukuwafuatafuata Walawi, watoze Wayuda na Wayerusalemu machango, aliyoyaagiza Mose, mtumishi wa Bwana, mkutano wa Waisiraeli wayachangie Hema la Ushahidi, kisha wayalete huku? Kwani wana wa Atalia, yule mwanamke aliyefanya maovu tu, wameichakaza Nyumba ya Mungu, navyo vyombo vitakatifu vyote vya Nyumba ya Bwana wakavifanya kuwa vya Mabaali, Kwa kuwa mfalme aliviagiza, wakatengeneza kasha moja, wakaliweka nje langoni penye Nyumba ya Bwana, wakapiga mbiu katika nchi ya Yuda namo Yerusalemu, watu wamletee Bwana machango, Mose, mtumishi wa Mungu, aliyoyaagiza kule nyikani, Waisiraeli wayatoe. Wakuu wote na watu wote wakafurahi, wakayaleta, wakayatia mle kashani, hata wakalijaza. Ikawa, palipotimia pa kulipeleka hilo kasha kwa wasimamizi wa mfalme, likachukuliwa na Walawi; ilikuwa hapo, walipoona, ya kuwa zimo fedha nyingi, Kisha akaja mwandishi wa mfalme na msimamizi wa mtambikaji mkuu, wakatoa fedha zote zilizokuwamo kashani, kisha wakalichukua, wakalirudisha mahali pake siku kwa siku. Ndivyo, walivyokusanya fedha nyingi. Mfalme na Yoyada wakawapa mafundi wa kazi za kuitengeneza Nyumba ya Bwana; nao wakajitafutia waashi na maseremala wa kuirudishia Nyumba ya Bwana upya, hata wafua vyuma na shaba wa kuitengenezatengeneza Nyumba ya Bwana. Hao mafundi wakazifanya kazi zao, kwa kazi za mikono yao matengenezo yakaendelea, wakaisimamisha Nyumba ya Bwana kuwa, kama ilivyokuwa, wakaishupaza. Walipokwisha wakazipeleka fedha zilizobaki kwa mfalme na kwa Yoyada, wakazitumia kutengeneza vyombo vya Nyumba ya Bwana, ni vyombo vya kutumia, walipotoa ng'ombe za tambiko, na vyano na vyombo vingine vya dhahabu na vya fedha, kisha wakamtolea Bwana katika Nyumba ya Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima pasipo kukoma siku zote za Yoyada. Yoyada alipokuwa mzee wa kushiba siku, akafa; akawa mwenye miaka 130 alipokufa. Wakamzika mjini mwa Dawidi penye wafalme, kwani aliwafanyizia Waisiraeli mema kwa kuyatengeneza mambo ya Mungu na ya Nyumba yake. Yoyada alipokwisha kufa, wakuu wa Wayuda wakaja, wakamwangukia mfalme; ndipo, mfalme alipowasikia. Wakaiacha Nyumba ya Bwana Mungu wa baba zao, wakaitumikia miti ya Ashera na nguzo za kutambikia; ndipo, Mungu alipoikasirikia nchi ya Yuda na Yerusalemu kwa kuzikora hizo manza, akatuma kwao wafumbuaji, wawarudishe kwake Bwana, lakini hawakuwasikiliza. Ndipo, roho ya Mungu ilipomwingia Zakaria, mwana wa mtambikaji Yoyada, akaja kusimama mbele ya watu mahali palipokuwa juu kidogo, akawaambia: Hivi ndivyo, Mungu anavyosema: Mbona mnayaacha maagizo ya Bwana, msiendelee kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana, naye amewaacha. Ndipo, walipomlia njama, wakamwua kwa kumpiga mawe uani penye Nyumba ya Bwana kwa kuagizwa na mfalme. Ndipo, mfalme Yoasi alipoacha kuyakumbuka matendo yote ya upole, baba yake Yoyada aliyomfanyizia, naye akamwua mwanawe; huyu alipokufa akasema: Bwana na ayaone na kuyalipisha! Ikawa, mwaka ulipokwisha, vikapanda vikosi vya Washami, kupigana naye, wakaja kuiingia nchi ya Yuda, hata Yerusalemu, wakawaangamiza wakuu wote wa watu wote pia, nayo mateka yao wakayatuma kwa mfalme wa Damasko. Kweli hivyo vikosi vya Ushami vilikuja vyenye watu wachache tu, lakini Bwana akatia mikononi mwao vikosi vilivyokuwa vyenye watu wengi sana, kwa kuwa walimwacha Bwana Mungu wa baba zao; ndivyo, walivyompatiliza Yoasi. Walipokwenda zao, wakamwacha mwenye magonjwa mengi; ndipo, watumishi wake walipomlia njama, kwa kuwa alizimwaga damu za wana wa mtambikaji Yoyada, wakamwua kitandani pake, akafa; kisha wakamzika mjini mwa Dawidi, lakini hawakumzika penye makaburi ya wafalme. Waliomlia njama ndio hawa: Zabadi, mwana wa Simati aliyekuwa mwanamke wa Kiamoni, na Yozabadi, mwana wa Simuriti aliyekuwa mwanamke wa Kimoabu. Mambo ya wanawe na yale ya machango mengi, aliyoyachangisha, na majengo ya kuijenga tena Nyumba ya Mungu, tunayaona, yameandikwa katika maelezo ya kitabu cha matendo ya wafalme. Naye mwanawe Amasia akawa mfalme mahali pake. Amasia alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 29 mle Yerusalemu. Jina la mama yake ni Yoadani wa Yerusalemu. Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana, lakini hakuyafanya kwa moyo wote mzima. Ikawa, alipoushupaza ufalme wake, akawaua watumishi wake waliomwua baba yake mfalme. Lakini wana wao hakuwaua, kwa kuwa katika Maonyo katika kitabu cha Mose imeandikwa, ya kuwa Bwana ameagiza kwamba: Baba wasife kwa ajili ya wana, wala wana wasife kwa ajili ya baba, ila kila mtu sharti afe kwa kosa lake yeye. Kisha Amasia akawakusanya Wayuda, akawapanga kwa milango na kwa wakuu wa maelfu na kwa wakuu wa mamia wote pia waliokuwa Wayuda na Wabenyamini. Alipowakagua walio wenye miaka ishirini na zaidi akapata watu 300000 waliochaguliwa kwenda vitani waliojua kushika mikuki na ngao. Akajipatia nako kwa Waisiraeli watu wa mshahara 100000 waliokuwa mafundi wa vita wenye nguvu, akawalipa vipande mia vya fedha, ndio shilingi milioni na 200000. Ndipo, mtu wa Mungu alipomjia, akamwambia: Mfalme, vikosi vya Waisiraeli visiende na wewe! Kwani Bwana hawi nao Waisiraeli, maana wote ni wana wa Efuraimu. Kama ni kwenda, vifanye wewe, ukijishupaza, upate kupigana! Kama sivyo, Mungu atakukwaza mbele ya adui, kwani Mungu anazo nguvu za kusaidia na za kukwaza. Amasia akamwuliza huyu mtu wa Mungu: Tena nivifanyeje vile vipande mia vya fedha, nilivyowapa wao wa kikosi cha Waisiraeli? Ndipo, huyu mtu wa Mungu alipomwambia: Bwana anaweza kukupa zaidi ya hivyo. Kisha Amasia akakitenga kile kikosi kilichokuja kwake toka nchi ya Efuraimu, waende kwao; nao wakawakasirikia sana Wayuda, wakarudi kwao wenye makali yaliyowaka moto. Kisha Amasia akajishupaza, akawaongoza watu wake kwenda katika Bonde la Chumvi, akawapiga wana wa Seiri 10000, wengine 10000 wana wa Yuda wakawateka, wa hai, wakawapeleka mwambani juu, wakawakumba toka hapo juu mwambani; ndipo, wote pia walipopondeka. Lakini watu wa kile kikosi, Amasia alichokirudisha, wasiende naye kupigana, waliingia miji ya Yuda toka Samaria hata Beti-Horoni, na kunyang'anya mali, wakapiga humo watu 3000, wakachukua mali nyingi, walizozinyang'anya. Amasia aliporudi akiisha kuwashinda Waedomu akaileta miungu ya wana wa Seiri, akaiweka kuwa miungu yake, akaiangukia na kuivukizia. Kwa hiyo Bwana akamkasirikia Amasia sana, akatuma mfumbuaji kwake, akamwambia: Mbona unaifuatafuata miungu ya watu hao, isiyowaponya watu wao mikononi mwako? Alipomwambia hayo, akamwuliza: Tumekuweka kula njama na mfalme? Yaache! Unatakiaje, wakupige? Ndipo, mfumbuaji alipoacha akisema: Ninajua sasa, ya kuwa Mungu anataka kukuangamiza, kwa sababu umefanya hivyo, usilisikie shauri langu. Kisha Amasia, mfalme wa Yuda, akapiga shauri, akatuma kwa Yoasi, mwana wa Yoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Waisiraeli, kumwambia: Njoo, tuonane uso kwa uso! Naye Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, akatuma kwa Amasia, mfalme wa Wayuda, kumwambia: Kingugi kilichoko Libanoni kilituma kwa mwangati ulioko Libanoni kwamba: Mpe mwanangu mtoto wako wa kike, awe mkewe! Ndipo, nyama wa porini wa huko Libanoni alipopita, akakikanyaga kile kingugi na kukiponda. Unasema, umewapiga Waedomu; kwa hiyo moyo wako unakukuza, ujitutumue. Sasa kaa nyumbani mwako! Mbona unataka kujitia katika vita vibaya, uanguke wewe na Wayuda pamoja na wewe? Lakini Amasia hakusikia, kwani jambo hilo limetoka kwa Mungu, awatie mikononi mwa wengine, kwa kuwa waliifuatafuata miungu ya Waedomu. Basi, Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, akapanda, wakaonana uso kwa uso, yeye na Amasia, mfalme wa Wayuda, huko Beti-Semesi katika nchi ya Wayuda. Wayuda wakashindwa na Waisiraeli, wakakimbia kila mtu hemani kwake. Naye Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, akamkamata Amasia, mfalme wa Yuda, aliyekuwa mwana wa Yoasi, mwana wa Yoahazi, kule Beti-Semesi, akampeleka Yerusalemu, akalivunja boma la Yerusalemu toka lango la Efuraimu hata lango la pembeni, ndio mikono 400. Akachukua dhahabu na fedha zote, navyo vyombo vyote vilivyopatikana Nyumbani mwa Mungu kwa Obedi-Edomu navyo vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme nao watu, aliowataka kuwa kole, kisha akarudi Samaria. Ikawa, Yoasi, mwana wa Yoahazi, mfalme wa Isiraeli, alipokwisha kufa, Amasia, mwana wa Yoasi, mfalme wa Wayuda, akawapo tena miaka 15. Mambo mengine ya Amasia, ya mwanzo na ya mwisho, hatuyaoni, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Wayuda na wa Waisiraeli? Tangu hapo, Amasia alipoacha kumfuata Bwana, walikuwako watu huko Yerusalemu waliomlia njama ya kumwua; kwa hiyo akakimbilia Lakisi, lakini wale wakatuma watu kumfuata lakisi, nao wakamwua huko. Wakamchukua kwa farasi, wakamzika kwa baba zake mjini mwa Yuda. Watu wote wa Yuda wakamchukua Uzia aliyekuwa mwenye miaka 16, wakamfanya kuwa mfalme mahali pa baba yake Amasia. Yeye akaujenga Eloti, akaurudisha kwao Wayuda, mfalme alipokuwa amelala na baba zake. Uzia alikuwa mwenye miaka 16 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 52 mle Yerusalemu. Jina la mama yake ni Yekolia wa Yerusalemu. Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana, kama yote, baba yake Amasia aliyoyafanya. Akawa akimtafuta Mungu siku, alizokuwapo Zakaria aliyemfundisha maana ya kumtazamia Mungu; nazo siku zile, alipomtafuta Bwana, Mungu akayaendesha mambo yake. Akatoka, akapigana na Wafilisti, akalivunja boma la Gati na boma la Yabune na boma la Asdodi, akajenga miji kwao Waasdodi nako kwao Wafilisti. Mungu akamsaidia kuwashinda Wafilisti na Waarabu waliokaa Guri-Baali na Wameuni. Ndipo, Waamoni walipompa Uzia mahongo, jina lake likafika hata Misri, kwani alijipatia nguvu zaidi. Kisha Uzia akajenga minara huko Yerusalemu penye lango la pembeni napo penye lango la bondeni napo, boma lilipojipinda, akaitia nguvu. Hata nyikani akajenga minara, akachimba visima vingi, kwani alikuwa na makundi mengi katika nchi ya tambarare, nako kwenye mbuga; akawa na wakulima na watunza mizabibu milimani na mashambani kwenye wiva, kwani alipenda kazi za ulimaji. Tena Uzia alikuwa na vikosi vya wapiga vita waliotoka kupigana, kila kimoja chenye hesabu ya watu waliokaguliwa na mwandishi Yieli na mwenye amri Masea kwa msaada wa Hanania aliyekuwa mkuu wa mfalme; hesabu yote ya wakuu wa milango ya mafundi wa vita ilikuwa 2600. Mikononi mwao vilikuwa vikosi vya askari, watu 307500 waliopiga vita kwa nguvu nyingi, wamsaidie mfalme kushinda adui. Hivyo vikosi vyote Uzia akavipatia ngao na mikuki na kofia ngumu na shati za vyuma na pindi na mawe ya makombeo. Akatengeneza mle Yerusalemu makombeo makubwa, akitumia mafundi wenye mawazo ya kutunga matengenezo kama hayo, akayaweka juu ya minara, hata pembenipembeni ya kutupia mishale na mawe makubwa; kwa hiyo jina lake likafika hata katika nchi za mbali, kwani vikastaajabisha, alivyosaidiwa, akaendelea kupata nguvu. Alipopata nguvu, moyo wake ukajikuza, afanye yasiyofanywa, akamvunjia Bwana Mungu wake maagano akiingia Jumbani mwa Bwana kumvukizia mezani pa kuvukizia. Mtambikaji Azaria akamfuata pamoja na watambikaji wa Bwana 80 waliokuwa wenye nguvu. Wakajipanga, wamkinge mfalme Uzia wakimwambia: Siyo kazi yako, Uzia, kumvukizia Bwana, ila ni yao watambikaji walio wana wa Haroni, wametakaswa, wavukize. Toka Patakatifu, kwani umeyavunja maagano, kwani hutajipatia macheo kwa Bwana Mungu. Ndipo, Uzia alipochafuka, nacho kivukizio cha kuvukizia kilikuwa mkononi mwake; alipowatolea watambikaji machafuko yake, ukoma ukamtoka pajini pake usoni pa watambikaji mle Nyumbani mwa Bwana kando ya meza ya kuvukizia. Mtambikaji mkuu Azaria na watambikaji wote walipomgeukia, mara wakamwona kuwa na ukoma pajini; ndipo, walipomfukuza huko upesiupesi, naye akajihimiza kutoka, kwa kuwa Bwana amempiga. Mfalme Uzia akawa mwenye ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa akiwa mwenye ukoma katika nyumba ya wagonjwa waliotengwa, kwani alikatazwa kuiingia Nyumba ya Bwana, mwanawe Yotamu akawa mkuu nyumbani mwa mfalme, akawaamua watu wa nchi hii. Mambo mengine ya Uzia, ya mwanzo na ya mwisho, aliyaandika mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi. Uzia akaja kulala na baba zake, wakamzika kwa baba zake porini kwenye makaburi ya wafalme, kwani walisema: Huyu ni mkoma. Kisha mwanawe Yotamu akawa mfalme mahali pake. Yotamu alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 16 mle Yerusalemu. Jina la mama yake ni Yerusa, binti Sadoki. Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama yote, aliyoyafanya baba yake Uzia, namo Jumbani mwa Bwana hakuingia; lakini watu wakaendelea kuyafanya yasiyofanywa. Yeye ndiye aliyelijenga lango la juu la Nyumba ya Bwana, hata kuta za Ofeli akazijenga vema. Hata milimani katika nchi ya Yuda akajenga miji, nako miituni akajenga ngome na minara. Tena akapiga vita na mfalme wa wana wa Amoni akawashinda. Kwa hiyo wana wa Amoni hawakuwa na budi kumpa katika mwaka huo vipande 100 vya fedha, ndio shilingi milioni na 200000 na ngano frasila 100000 na mawele vilevile frasila 100000. Hata mwaka wa pili na wa tatu wana wa Amoni wakamtolea yayo hayo. Yotamu akendelea kupata nguvu, kwa kuwa njia zake, alizozishika, zilimwelekea Bwana Mungu wake. Mambo mengine ya Yotamu na vita vyake vyote na njia zake tunaziona, zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Waisiraeli na wa Wayuda. Alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 16 mle Yerusalemu. Kisha akaja kulala na baba zake, wakamzika mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Ahazi akawa mfalme mahali pake. Ahazi alikuwa mwenye miaka 20 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 16 mle Yerusalemu; hakuyafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama baba yake Dawidi, ila akaendelea kuzishika njia za wafalme wa Waisiraeli, akatengeneza navyo vinyago vya Mabaali vilivyoyeyushwa. Naye yeye akavukiza bondone kwa Bin-Hinomu, hata wanawe akawatumia kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa motoni akiyafuata hayo matapisho ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Isiraeli. Akatambika na kuvukiza vilimani pa kutambikia napo pengine palipoinukia juu, hata chini ya kila mti uliokuwa wenye majani mengi. Kwa hiyo Bwana akamtia mkononi mwa mfalme wa Ushami, wakampiga, wakateka kwake mateka mengi, wakawapeleka Damasko. Akatiwa hata mkononi mwa mfalme wa Waisiraeli aliyempiga pigo kubwa. Kwani Peka, mwana wa Remalia, akaua katika nchi ya Yuda siku moja watu 120000, wote walikuwa wenye nguvu, kwa kuwa walimwacha Bwana Mungu wa baba zao. Hata Zikiri, fundi wa vita wa Waefuraimu, akamwua Masea, mwana wa mfalme, na Azirikamu, mkuu wa nyumba ya mfalme, na Elkana aliyemfuata mfalme kwa ukuu. Nao wana wa Isiraeli wakateka kwa ndugu zao 200000, wanawake na watoto wa kiume na wa kike na mali nyingi, walizozinyang'anya kwao; haya mateka wakayapeleka Samaria. Huko kulikuwa na mfumbuaji wa Bwana, jina lake Odedi. Huyu akavitokea vile vikosi, vilipoingia Samaria, akawaambia: Tazameni! Kwa kuwa Bwana Mungu wa baba zenu amewakasirikia sana Wayuda, akawatia mikononi mwenu, lakini ninyi kwa machafuko mkamwaga kwao damu nyingi zilizofika hata mbinguni. Sasa ninyi mwataka kuwanyenyekeza kwa nguvu hawa wana wa Yuda na wa Yerusalemu, wawe watumwa na vijakazi wenu. Lakini nanyi mliyojipatia kwake Bwana Mungu wenu sizo manza tu, mlizozikora? Kwa hiyo nisikieni sasa, mrudishe kwao mateka, mliyoyateka kwa ndugu zenu! Kwani nanyi makali ya Bwana yawakayo moto yanawakalia. Ndipo, walipoinuka waume waliokuwa wakuu wa wana wa Efuraimu, ndio Azaria, mwana wa Yohana, Berekia, mwana wa Mesilemoti, na Hizikia, mwana wa Salumu, na Amasa, mwana wa Hadilai; hawa wakawainukia waliotoka vitani, wakawaambia: Msiyalete mateka yenu hapa! Kwani hivyo tutakora manza kwa Bwana, nanyi mnataka kweli kuyaongeza makosa yetu na manza zetu, kwani manza zetu ni nyingi, nayo makali yawakayo moto yanatukalia sisi Waisiraeli. Ndipo, wapiga vita walipoyaacha mateka yao machoni pao wakuu napo pao mkutano wote pamoja na zile mali, walizozinyang'anya; nao wale waume waliotajwa hapa juu majina yao wakainuka kuyachukua hayo mateka, kisha wote waliokuwa uchi wakawavika wakiwapa nguo na viatu na kuvitoa mlemle katika mapokonyo, kisha wakawapa vyakula na vya kunywa na mafuta ya kukipaka, nao wote waliojikwaakwaa wakawapandisha punda, wakawapeleka kwa ndugu zao Yeriko, ule mji wenye mitende, kisha wakarudi Samaria. Siku zile mfalme Ahazi akatuma kwao wafalme wa Asuri, waje kumsaidia, kwa maana Waedomu walikuja tena, wakawapiga, wakachukua mateka. Nao Wafilisti wakaiingia miji ya nchi ya tambarare na miji ya kusini katika nchi ya Yuda na kunyang'anya mali, wakateka Beti-Semesi na Ayaloni na Gederoti na Soko na mitaa yake na Timuna na mitaa yake na Gimuzo na mitaa yake, wakakaa humo. Kwani Bwana aliwanyenyekeza Wayuda kwa ajili ya Ahazi, mfalme wa Waisiraeli, kwani aliwalegeza Wayuda alipomvunjia Bwana maagano. Ndipo, Tilgati-Pilneseri, mfalme wa Asuri, alipomjia, lakini akamsonga, hakumpatia nguvu. Kwani Ahazi alichukua kwa nguvu yaliyokuwamo Nyumbani mwa Bwana namo nyumbani mwa mfalme nazo mali za wakuu, akampa mfalme wa Asuri, lakini hakusaidiwa naye. Papo hapo, aliposongeka, yeye mfalme Ahazi akazidi kumvunjia Bwana maagano, akaitumikia miungu ya Damasko iliyompiga, akasema: kwa kuwa miungu ya wafalme wa Ushami ndiyo iliyowasaidia, basi, nitaitambikia hiyohiyo, wanisadie; nayo ndiyo iliyomkwaza mwenyewe na Waisiraeli wote. Kisha Ahazi akavikusanya vyombo vya Nyumba ya Mungu, akavivunjavunja hivyo vyombo vya Nyumba ya Mungu, akaifunga milango ya Nyumba ya Bwana, akajitengenezea pa kutambikia pembeni po pote mle Yerusalemu. Hata kila mji mmoja wa Yuda akautengenezea vilima vya kuvukizia miungu mingine juu yao; ndivyo, alivyomkasirisha Bwana Mungu wa baba zake. Mambo yake mengine na njia zake zote, za kwanza na za mwisho, tunaziona, zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Wayuda na wa Waisiraeli. Kisha Ahazi akaja kulala na baba zake, wakamzika katika mji wa Yerusalemu, kwani hawakumpeleka penye makaburi ya wafalme wa Waisraeli. Naye mwanawe Hizikia akawa mfalme mahali pake. Hizikia akaupata ufalme alipokuwa mwenye miaka 25, akawa mfalme miaka 29 mle Yerusalemu. Jina la mama yake ni Abia, binti Zakaria. Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama yote, aliyoyafanya baba yake Dawidi. Katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake katika mwezi wa kwanza akaifungua milango ya Nyumba ya Bwana, akaitengeneza vema. Kisha akaleta watambikaji na Walawi, akawakusanya uwanjani upande wa maawioni kwa jua. Akawaambia: Nisikieni, ninyi Walawi! Sasa jieueni, mpate kuieua nayo Nyumba ya Bwana Mungu wa baba zenu na kuutoa uchafu hapa Patakatifu! Kwani baba zetu wameyavunja maagano, wakayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana Mungu wetu, wakamwacha na kuzigeuza nyuso zao, zisilitazame Kao la Bwana, wakalielekezea migongo. Wakaifunga nayo milango ya ukumbi, wakazizima taa zake, hawakumvukizia Mungu wa Isiraeli mavukizo, wala hawakumtolea ng'ombe za tambiko hapa Patakatifu. Kwa hiyo makali ya Bwana yakaikalia nchi ya Yuda na Yerusalemu, akawatoa, watupwe huko na huko, wastukiwe kabisa na kuzomewa, kama ninyi mnavyoviona wenyewe kwa macho yenu. Tazameni! Baba zetu waliuawa kwa panga, nao wana wetu wa kiume na wa kike pamoja na wanawake wetu wakatekwa kwa sababu hiyo. Sasa mimi nimejipa moyo, nifanye agano na Bwana Mungu wa Isiraeli, makali yake yawakayo moto yatuondokee. Sasa ninyi wanangu, msizurure! Kwani ninyi Bwana aliwachagua, msimame mbele yake na kumtumikia, mwe watumishi wake na wavukizaji wake. Ndipo, walipoinuka Walawi: Mahati, mwana wa Amasai, na Yoeli, mwana wa Azaria, walio wana wa Kehati; nao waliokuwa wana wa Merari: Kisi, mwana wa Abudi, na Azaria, mwana wa Yehaleleli, nao waliokuwa wana wa Gersoni: Yoa, mwana wa Zima, na Edeni, mwana wa Yoa; nao waliokuwa wana wa Elisafani: Simuri na Yieli; nao waliokuwa wana wa Asafu: Zakaria na Matania; nao waliokuwa wana wa Hemani: Yehieli na Simei; nao waliokuwa wana wa Yedutuni: Semaya na Uzieli. Wakawakusanya ndugu zao, wakajieua; kisha wakaja kwa agizo la mfalme kuitakasa Nyumba ya Bwana, kama Bwana alivyosema. Watambikaji wakaingia Nyumbani mwa Bwana ndani kuitakasa na kuyatoa machafu yote, waliyoyaona Jumbani mwa Bwana, wakayapeleka uani penye Nyumba ya Bwana; ndiko, Walawi walikoyachukua, wayapeleke nje mtoni kwa Kidoroni. Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wakaanza kuitakasa, siku ya nane ya huo mwezi wakafika penye ukumbi wa Bwana, wakaitakasa Nyumba ya Bwana tena siku nane, wakaimaliza siku ya kumi na sita ya mwezi wa kwanza. Kisha wakaingia nyumbani kwa mfalme Hizikia, wakamwamiba: Tumeitakasa Nyumba yote ya Bwana, hata meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko na vyombo vyake vyote,, hata meza ya mikate, aliyowekewa Bwana, na vyombo vyake vyote. Navyo vyombo vyote, mfalme Ahazi alivyovichafua katika ufalme wake, alipoyavunja maagano, tumevitengeneza na kuvitakasa, utaviona, viko mbele ya meza ya kumtambikia Bwana. Ndipo, mfalme Hizikia alipoamka na mapema, akawakusanya wakuu wa mji, akapanda kwenda Nyumbani kwa Bwana. Wakaleta madume saba ya ng'ombe na madume saba ya kondoo na wana kondoo saba na madume saba ya mbuzi kuwa ng'ombe za tambiko za weuo kwa ajili ya ufalme na kwa ajili ya Patakatifu na kwa ajili ya Wayuda. Akawaambia watambikaji, wana wa Haroni, wawatoe kuwa ng'ombe za tambiko hapo pa kumtambikia Bwana. Ndipo, walipowachinja hao ng'ombe, nao watambikaji wakazichukua damu zao, wakazinyunyizia meza ya kutambikia; wakawachinja nao madume ya kondoo, nazo damu zao wakazinyunyizia meza ya kutambikia, wakawachinja nao wana kondoo, nazo damu zao wakazinyunyizia meza ya kutambikia. Kisha wakawapeleka madume ya mbuzi ya weuo mbele ya mfalme na mbele ya huo mkutano, wakawabandikia mikono yao. Kisha watambikaji wakawachinja, nazo damu zao wakazinyunyizia meza ya Bwana kuwa mweuo wa kuwapatia Waisiraeli wote upozi, kwani mfalme aliagiza kwa ajili ya Waisiraeli wote kutoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za weuo. Naye alikuwa amewasimamisha Walawi penye Nyumba ya Bwana, wakiyashika matoazi na mapango na mazeze, kama Dawidi na Gadi aliyekuwa mchunguzaji wa mfalme na mfumbuaji Natani walivyoviagiza; kwani agizo hilo lilitoka kwa Bwana, likatokea vinywani mwa wafumbuaji wake. Kwa hiyo Walawi wakasimama na kuvishika vyombo vya Dawidi, nao watambikaji wakashika matarumbeta. Hizikia alipoagiza kuziteketeza ng'ombe za tambiko mezani pa kutambikia, papo hapo tambiko lilipanzia, ndipo, wimbo wa Bwana ulipoanzia pamoja na matarumbeta yaliyoongozwa na vyombo vya Dawidi, mfalme wa Waisiraeli. Mkutano wote pia ukamwangukia Bwana, wimbo ulipoimbwa, nayo matarumbeta yalipolia; yote yakawa hivyo, hata ng'ombe za tambiko zikaisha kuteketezwa. Walipokwisha kuziteketeza hizo ng'ombe za tambiko, wakapiga magoti, yeye mfalme nao wote waliokuwako naye, wakamwangukia Bwana. Kisha mfalme Hizikia na wakuu wakawaambia Walawi, wamtukuze Bwana na kuyaimba maneno ya Dawidi na ya mchunguzaji Asafu. Ndipo, walipomtukuza kwa furaha, kisha wakainama, wakamwangukia. Kisha Hizikia akawaitikia akisema: Sasa mmeyajaza magao yenu kumtumikia Bwana, basi, karibuni, mlete huku kwenye Nyumba ya Bwana ng'ombe za tambiko na vipaji vya shukrani! Ndipo, watu wa huo mkutano walipoleta ng'ombe za tambiko na vipaji vya shukrani, kila mtu akatoa ng'ombe za tambiko, kama moyo ulivyopenda. Hesabu ya ng'ombe za tambiko, watu wa huo mkutano walizozitoa, ikawa ng'ombe 70, madume ya kondoo 100, wana kondoo 200; hawa wote walikuwa wa kumteketezea Bwana. Tena za matambiko mengine wakatolewa ng'ombe 600 na kondoo na mbuzi 3000. Watambikaji tu walikuwa wachache, hawakuweza kuwachuna ng'ombe wote wa kuteketezwa, kwa hiyo ndugu zao Walawi wakawasaidia, mpaka kazi hii ikaisha, tena mpaka watambikaji wakajieua, kwani Walawi walikuwa wenye mioyo iliyojihimiza kujieua kuliko yao watambikaji. Nao ng'ombe wa kuteketezwa nzima walikuwa wengi, vilevile vipande vyenye mafuta ya ng'ombe za tambiko za shukurani na vinywaji vya tambiko vilivyopasa kila ng'ombe ya tambiko. Ndivyo, utumishi wa Nyumbani mwa Bwana ulivyotengenezwa tena. Hizikia na watu wote wakafurahi kwa hayo, Mungu aliyowatengenezea watu, kwani jambo hili lilifanyika kwa upesi sana. Hizikia akatuma kwa Waisiraeli na kwa Wayuda wote, nao Waefuraimu na Wamanase akawaandikia barua, waje Yerusalemu Nyumbani mwa Bwana Mungu wa Isiraeli kula sikukuu ya Pasaka ya Bwana Mungu wa Isiraeli. Mfalme na wakuu wake nao mkutano wote wa watu wakafanya shauri huko Yerusalemu kula sikukuu ya Pasaka katika mwezi wa pili. Kwani hawakuweza kuila siku zile, kwa kuwa watambikaji wa kutosha hawajajieua, nao watu hawakukusanyika Yerusalemu. Shauri hili likanyoka machoni pake mfalme napo pao mkutano wote. Wakaagiza kupiga mbiu kwa Waisiraeli wote toka Beri-Seba hata Dani, watu waje kula sikukuu ya Pasaka ya Bwana Mungu wa Isiraeli mle Yerusalemu, kwani tangu siku nyingi hawakuila, kama ilivyoandikwa. Wajumbe wapigao mbio wakaenda na barua, walizopewa na mfalme na wakuu wake, katika nchi zote za Waisiraeli na za Wayuda, wakasema, kama walivyoagizwa na mfalme: Wana wa Isiraeli rudini kwake Bwana, Mungu wa Aburahamu na wa Isaka na wa Isiraeli! Ndipo, atakaporudi kwao waliosalia kwenu kwa kupona mikononi mwa wafalme wa Asuri. Msiwe kama baba zenu na ndugu zenu walioyavunja maagano ya Bwana Mungu wa baba zao, akawatoa, waangamizwe, kama mnavyoona nanyi. Sasa msizishupaze kosi zenu kama baba zenu! Ila mpeni Bwana mikono mkija Patakatifu pake, alipopatakasa kuwa pake kale na kale! Kamtumikieni Bwana Mungu wenu! Ndipo, makali yake yawakayo moto yatakapoondoka kwenu. Kwani mkirudi kwake Bwana, ndugu zenu na wana wenu watahurumiwa nao waliowateka na kuwahamisha, wapate kurudi katika nchi hii, kwani Bwana Mungu wenu ni mwenye utu na huruma, hatauondoa uso kwenu, mkirudi kwake. Basi, hao wajumbe wapigao mbio wakaenda kuingia mji kwa mji katika nchi ya Efuraimu na ya Manase hata Zebuluni, lakini watu wakawacheka na kuwafyoza. Watu wa Aseri tu na wa Manase na wa Zebuluni wakajinyenyekeza, wakaja Yerusalemu. Hata katika nchi ya Yuda mkono wa Mungu ukawako, ukawapa kuwa wenye moyo mmoja wa kulifanya agizo la mfalme na la wakuu, Bwana alilowaambia. Katika mwezi wa pili wakakusanyika Yerusalemu watu wengi kuila sikukuu ya Mikate isiyochachwa, ukawa mkutano mkubwa sana. Wakainuka, wakapaondoa pote pa kutambikia palipokuwamo Yerusalemu, navyo vivukizo vyote wakaviondoa, wakavitupa katika mto wa Kidoroni. Kisha wakachinja wana kondoo wa Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili, kwani watambikaji na Walawi walijieua kwa kuona soni, wakapeleka ng'ombe za tambiko Nyumbani mwa Bwana. Wakasimama mahali pao palipowapasa, kama Maonyo ya Mose aliyekuwa mtu wa Mungu yalivyoagiza. Hao watambikaji wakazinyunyiza damu, walizozipokea mikononi mwa Walawi. Kwani katika huo mkutano walikuwako wengi wasiojieua; kwa sababu hii Walawi wakawachinjia wote wasiotakata wana kondoo wa Pasaka, wawatakase kuwa wa Bwana. Kwani watu wengi sana wa Efuraimu na wa Manase na wa Isakari na wa Zebuluni hawakujitakasa, kwani hawakuila kondoo ya Pasaka, kama ilivyoandikwa. Lakini Hizikia aliwaombea kwamba: Bwana aliye mwema na amwondolee makosa kila mtu aliyeuelekeza moyo wake kumtafuta Mungu Bwana aliye Mungu wa baba zake, ingawa hakuupata utakaso upapasao Patakatifu. Bwana akamsikia Hizikia, akawaponya hao watu. Ndivyo, wana wa Isiraeli waliokuwamo Yerusalemu walivyoila sikukuu ya Mikate isiyochachwa siku saba kwa furaha kubwa, nao Walawi na watambikaji wakamshangilia Bwana siku kwa siku na kumpigia Bwana vyombo vyenye sauti za nguvu. Naye Hizikia akawaambia Walawi wote waliokuwa wenye akili njema katika kazi ya Bwana maneno yaliyoingia mioyoni mwao, wakaila sikukuu hii ya ushahidi siku saba, wakitoa vipaji vya tambiko vya shukrani, wamshukuru Bwana Mungu wa baba zao. Kisha mkutano wote ukafanya shauri kuendelea siku saba tena, wakala sikukuu tena siku saba kwa furaha. Kwani Hizikia, mfalme wa Wayuda, aliutolea huo mkutano madume ya ng'ombe 1000 na mbuzi na kondoo 7000, nao wakuu waliutolea mkutano madume ya ng'ombe 1000 na mbuzi na kondoo 7000; nao watambikaji walijieua wengi. Wakafurahi watu wote wa huo mkutano wa Wayuda pamoja na watambikaji na Walawi na mkutano wao wote waliotoka kwa Waisiraeli nao wageni waliotoka katika nchi ya Waisiraeli nao waliokaa katika nchi ya Wayuda. Ikawa furaha kubwa mle Yerusalemu, kwani tangu siku za Salomo, mwana wa Dawidi, mfalme wa Waisiraeli, haya kuwamo mle Yerusalemu mambo kama hayo. Mwisho watambikaji na Walawi wakainuka, wakawabariki watu; sauti zao zikasikiwa, nayo maombo yao yakafika mbinguni kwenye Kao lake takatifu. Walipokwisha kuyamaliza hayo yote, Waisiraeli wote waliokuwako wakatoka kwenda zao katika miji ya Yuda, wakazivunja nguzo za kutambikia, wakaikatakata nayo miti ya Ashera, wakavibomoa vijumba vya kutambikia vilimani pamoja na meza zao za kutambikia katika nchi zote za Yuda na za Benyamini na za Efuraimu na za Manase, mpaka wakavitowesha kabisa hivyo vyote, kisha wana wote wa Isiraeli wakarudi kila mtu mahali palipokuwamali yake katika miji yao. Kisha Hizikia akaweka kazi za zamu za watambikaji na za Walawi zizipasazo zamu zao, kila mtu akawa na kazi yake ya utumishi wake, watambikaji na Walawi: kuteketeza ng'ombe za tambiko na kutengeneza ng'ombe za tambiko za shukrani na kutumikia malangoni kwa matuo yake Bwana na kumshukuru na kumshangilia. Akayaweka nayo yampasayo mfalme kuyatoa katika mali zake kuwa ng'ombe za tambiko za asubuhi na za jioni na za matambiko ya siku za mapumziko na ya miandamo ya mwezi na ya sikukuu, kama ilivyoandikwa katika Maonyo ya Bwana. Tena akawaagiza watu waliokaa Yerusalemu kuwapa watambikaji na Walawi yawapasayo, wapate kuyashika Maonyo ya Bwana. Agizo hili lilipoenea, wana wa Isiraeli wengi wakaleta malimbuko ya ngano na ya mvinyo na ya mafuta na ya asali na ya mazao yote ya mashamba, wakayaleta nayo mafungu ya kumi ya mali zote, yakawa mengi. Nao wana wa Isiraeli na wa Yuda waliokaa katika miji ya Yuda wakaleta nayo mafungu ya kumi ya ng'ombe na ya mbuzi na ya kondoo nayo mafungu ya kumi ya vipaji vitakatifu vilivyotolewa kuwa mali za Bwana Mungu wao, wakaviweka machungu machungu. Katika mwezi wa tatu walianza kuyaweka hayo machungu, wakayamaliza katika mwezi wa tisa. Ndipo, Hizikia na wakuu walipokuja kuyatazama hayo machungu, wakamtukuza Bwana nao Waisiraeli walio ukoo wake. Hizikia alipoulizana na watambikaji na Walawi maana ya hayo machungu, Azaria aliyekuwa mtambikaji mkuu wa mlango wa Sadoki akamjibu, akamwambia: Tangu hapo, walipoanza kuyaleta haya matoleo Nyumbani mwa Bwana, tumekula na kushiba, nayo haya mengi ndiyo yaliyosalia, kwani Bwana amewabariki walio ukoo wake, kwa hiyo vimesalia hivyo vipaji vingi mno. Ndipo, Hizikia alipoagiza, watengeneze vyumba katika Nyumba ya Bwana: walipokwisha kuvitengeneza, wao kwa kuwa welekevu wakaingiza humo yale matoleo na mafungu ya kumi na vipaji vitakatifu vyote pia, Mlawi Konania akawekwa kuyaangalia, naye ndugu yake Simei akawa wa pili. Nao Yehieli na Azazia na Nahati na Asaheli na Yerimoti na Yozabadi na Elieli na Isimakia na Mahati na Benaya wakawekwa kuwa wasimamizi kumsaidia Konania na ndugu yake Simei kwa agizo lake mfalme Hizikia na Azaria aliyekuwa mwenye amri Nyumbani mwa Mungu. Tena Mlawi Kore, mwana wa Imuna, aliyelilinda lango lililoelekea maawioni kwa jua akawekwa kuviangalia vipaji vya Mungu, watu walivyovitoa kwa kupenda kwao wenyewe, agawe yaliyo matoleo ya Bwana nayo yaliyo matakatifu yenyewe. Waliomsaidia katika miji ya watambikaji ni Edeni na Minyamini na Yesua na Semaya na Amaria na Sekania, wawagawie kwa kweli ndugu zao yawapasayo kwa zamu zao, mkubwa kwa mdogo, kuliko wale wanawaume walioandikwa katika kitabu chao walio wa miaka mitatu na zaidi; nao hawa ndio wote waingiao Nyumbani mwa Bwana kwa mambo ya kila siku moja kufanya kazi za utumishi wao ziwapasazo kuziangalia kwa zamu zao. Katika kile kitabu cha udugu wa watambikaji imeandikwa milango ya baba zao, nacho cha Walawi kimeandikwa walio wenye miaka ishirini na zaidi kwa kazi zao ziwapasazo kuziangalia kwa zamu zao. Humo katika kitabu cha udugu wakaandikwa nao watoto wao wadogo wote na wake zao na wana wao wa kiume na wa kike wa mkutano wote pia, kwani kwa kuwa welekevu walijitakasa kuwa watakatifu kweli. Nao wana wa Haroni waliokuwa watambikaji mashambani kwenye mitaa ya miji yao wakapata watu katika kila mji mmoja walioandikwa majina yao, wawagawie yawapasayo, kila mume mmoja fungu lake miongoni mwa watambikaji, namo mwa Walawi wote walioandikwa katika kitabu cha udugu. Ndivyo, Hizikia alivyofanya katika nchi yote ya Yuda, akayafanya yaliyokuwa mema na manyofu na ya kweli machoni pake Bwana Mungu wake. Nazo kazi zote, alizozianza za kuitumikia Nyumba ya Mungu na za kuyafuata Maonyo na maagizo, kwa hivyo, alivyomtafuta Mungu, akazifanya kwa moyo wake wote, akafanikiwa. Hayo yalipokwisha kufanyika kwa welekevu, akaja Saniheribu, mfalme wa Asuri; akaingia katika nchi ya Yuda, akapiga makambi kwenye miji yenye maboma, akataka kujipenyeza humo, iwe yake. Hizikia alipoona, ya kuwa Saniheribu amekuja na kuuelekeza uso wake kuja kupiga vita Yerusalemu, akafanya shauri na wakuu wake na mafundi wake wa vita kuyaziba maji ya chemchemi zilizoko nje ya mji, nao wakamsaidia. Wakakusanyika watu wengi, wakaziziba chemchemi zote, hata kijito kilichopita katikati ya nchi hiyo wakisema: Mbona tuache, wafalme wa Asuri wakifika waone maji mengi? Akakaza kuutengeneza ukuta wote wa boma na kuujenga tena hapo, ulipobomoka, hata minara akaipandisha kwenda juu zaidi, nao ukuta wa pili wa nje akaujenga tena, hata ngome ya mji wa Dawidi akaitia nguvu, akatengeneza mata na ngao nyingi. Nao watu akawawekea wakuu wa vita, akawakusanya kwake uwanjani penye lango la mji, akawashikiza mioyo akiwaambia: Jipeni mioyo, mpate nguvu! Msiogope, wala msiingiwe na vituko mkimwona mfalme wa Asuri nao wale watu wengi mno, alio nao wote! Kwani walio upande wetu ndio wengi kuliko wao walio upande wake. Yeye anayo mikono yenye nyama, lakini sisi tunaye Bwana Mungu wetu kuwa msaada wetu kwa kutupigania mapigano yetu. Nao watu wakashikizwa na haya maneno ya Hizikia, mfalme wa Yuda. Baada ya hayo Saniheribu, mfalme wa Asuri, alipokuwa Lakisi pamoja na utukufu wake wote akatuma watumishi wake kwenda Yerusalemu kwa Hizikia, mfalme wa Wayuda, na kwa Wayuda wote waliokuwamo Yerusalemu kuwaambia: Hivi ndivyo, anavyosema Saniheribu, mfalme wa Asuri: Ninyi mnaegemea nini mkikaa ngomeni Yerusalemu na kusongwa? Je? Siye Hizikia anayewaponza na kuwatoa, mfe kwa njaa na kwa kiu akiwaambia: Bwana Mungu wetu atatuponya mkononi mwa mfalme wa Asuri? Huyu Hizikia siye aliyewakataza watu kumtambikia pake pa kutambikia vilimani napo penye meza zake za kutambikia akiwaambia Wayuda na Wayerusalemu kwamba: Sharti mmwangukie mbele ya meza moja tu ya kumtambikia na kumvukizia hapo tu? Hamyajui, mimi na baba zangu tuliyoyafanyia makabila yote ya nchi hizo? Je? Miungu yao mataifa ya nchi hizi iliweza kweli kuziponya nchi zao mikononi mwangu? Katika miungu yote ya haya mataifa, baba zangu waliyoyatia mwiko wa kuwapo, ulikuwa upi ulioweza kuwaponya watu wake mkononi mwangu? Naye Mungu wenu atawezaje kuwaponya mkononi mwangu? Sasa Hizikia asiwadanganye na kuwaponza ninyi kwa maneno kama hayo! Msimtegemee! Kwani hakuna mungu wo wote wa taifa au ufalme wo wote ulioweza kuwaponya watu wake mkononi mwangu wala mikononi mwa baba zangu. Sembuse Mungu wenu atawezaje kuwaponya mkononi mwangu? Yako na mengine, watumishi wake waliyoyasema ya kumkataa Bwana Mungu na mtumishi wake Hizikia. Akaandika nazo barua za kumfyoza Bwana Mungu wa Isiraeli, akisema humo kwamba: Kama miungu ya mataifa ya nchi hizi isivyoweza kuwaponya watu wao mkononi mwangu, vivyo hivyo naye Mungu wa Hizikia hataweza kuwaponya watu wake mkononi mwangu. Nao wa Yerusalemu waliokuwa ukutani juu wakawaambia haya Kiyuda na kuzipaza sana sauti zao, wawaogopeshe na kuwastusha, wapate kuuteka mji huu. Mambo ya Mungu wa Yerusalemu wakayawazia kuwa kama mambo ya miungu ya makabila mengine ya nchi hii iliyokuwa kazi za mikono ya watu tu. Ndipo, mfalme Hizikia na mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi, walipoomba kwa ajili ya hayo na kumlilia Alioko mbinguni. Bwana akatuma malaika wake, akaangamiza katika makambi ya mfalme wa Asuri mafundi wa vita wote waliokuwa wenye nguvu na wenye amri na wakuu, naye yeye hakuwa na budi kurudi kwao na kuuinamisha uso chini kwa soni. Alipoingia nyumbani mwa mungu wake, ndipo, wanawe wengine waliozaliwa naye mwenyewe walipomwua kwa upanga. Ndivyo, Bwana alivyomwokoa Hizikia na wenyeji wa Yerusalemu mkononi mwa Saniheribu, mfalme wa Wasuri, namo mikononi mwao wote wengine akiwalinda pande zote. Watu wengi wakamtolea Bwana vipaji na kuvipeleka Yerusalemu, naye Hizikia, mfalme wa Wayuda, wakampa matunzo, naye tangu hapo akatukuka sana machoni pao wamizimu wote. Siku hizo Hizikia akaugua, kufa kukamjia karibu sana; alipomlalamikia Bwana, huyu akasema naye na kumtolea kielekezo. Lakini Hizikia hakuyarudisha hayo mema aliyofanyiziwa, kwa kuwa moyo wake ulijikuza. Kwa hiyo makali ya Bwana yakaja kumkalia yeye, hata Wayuda na Wayerusalemu. Lakini Hizikia kwa hivyo, moyo wake ulivyojikuza, akajinyenyekeza tena yeye pamoja na wenyeji wa Yerusalemu; kwa sababu hii makali ya Bwana hayakuwatokea siku za Hizikia. Hizikia akawa mwenye mali na macheo mengi, akajipatia vilimbiko vya fedha na vya dhahabu na vya vito vyenye kima na vya manukato na vya ngao na vya vyombo vyo vyote, alivyovitamani, hata mawekeo ya mazao ya ngano na ya mvinyo mbichi na ya mafuta, hata mabanda ya nyama wote wa kufuga na makundi mazizini. Akajenga hata miji, kwani alikuwa na mbuzi na kondoo na ng'ombe wengi, kwani Mungu alimpa kupata mali nyingi sana. Naye Hizikia ndiye aliyeliziba tokeo la juu la maji ya kijito cha Gihoni na kuyapeleka moja kwa moja, yaushukie mji wa Dawidi upande wa machweoni kwa jua. Ndivyo, Hizikia alivyofanikiwa katika kazi zote. Hapo tu, wakuu wa Babeli walipotuma wasemaji kwake wa kuuliza maana ya kielekezo kilichofanyika katika nchi hii, Mungu alimwacha, amjaribu, ayajue yote yaliyokuwa moyoni mwake. Mambo mengine ya Hizikia nayo matendo ya upole wake tunayaona, yameandikwa katika maono ya mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi, na katika kitabu cha wafalme wa Wayuda na wa Waisiraeli. Hizikia alipokwenda kulala na baba zake, wakamzika pa kupandia penye makaburi ya wana wa Dawidi; Wayuda wote na wenyeji wa Yerusalemu wakamheshimu sana, alipokufa. Naye mwanawe Manase akawa mfalme mahali pake. Manase alikuwa mwenye miaka 12 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 55 mle Yerusalemu. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kwa kuyafuata matapisho ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Isiraeli. Akavijenga tena vijumba vya kutambikia vilimani, baba yake Hizikia alivyovibomoa, akaweka hata meza za kutambikia Mabaali, akatengeneza navyo vinyago vya Ashera, akaviangukia vikosi vyote vya mbinguni na kuvitumikia. Namo Nyumbani mwa Bwana akajenga penginepengine pa kutambikia, naye Bwana alisema: Yerusalemu ndimo, Jina langu litakamokaa. Katika nyua zote mbili za Nyumba ya Bwana akajenga pa kuvitambikia vikosi vyote vya mbinguni. Hata wanawe akawatumia kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa motoni katika Bonde la Bin-Hinomu; tena akaagulia mawingu, akapiga bao, tena akafanya uchawi, akatumia nao wakweza mizimu na wapunga pepo; akazidi kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, amkasirishe. Nacho kinyago cha kuchora, alichokitengeneza, akakiweka katika Nyumba ya Mungu, ambayo Mungu alimwambia Dawidi na mwanawe Salomo: Humu Nyumbani namo Yerusalemu, niliouchagua katika mashina yote ya Isiraeli, nitalikalisha Jina langu kale na kale. Sitaiondoa tena miguu ya Waisiraeli katika nchi hii, niliyowawekea baba zenu, wao wakijiangalia tu na kuyafanya yote, niliyowaagiza kinywani mwa Mose kuwa Maonyo na maongozi na maamuzi. Lakini Manase akawaponza Wayuda na wenyeji wa Yerusalemu kufanya mabaya kuliko wamizimu, Bwana aliowaangamiza mbele ya wana wa Isiraeli. Bwana akasema na Manase na watu wake, lakini hawakusikiliza. Kisha Bwana akawaletea wakuu wa vikosi vya mfalme wa Asuri, wakamkamata Manase kwa vyuma vyenye kulabu, wakamfunga kwa mapingu, wakampeleka Babeli. Aliposongeka hivyo akaulalamikia uso wa Bwana Mungu wake na kujinyenyekeza sana mbele ya Mungu wa baba zake. Alipomlalamikia hivyo na kumlilia, akayasikia maombo yake, akamrudisha Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo, Manase alipotambua, ya kuwa Bwana ndiye Mungu. Baada ya hayo akaujenga ukuta wa nje wa mji wa Dawidi ulioko upande wa machweoni kwa jua kulielekea bonde la kijito cha Gihoni mpaka kufika penye lango la Samaki na kuzunguka Ofeli, akaupandisha kwenda juu sana. Tena akaweka wakuu wa vikosi katika miji yote yenye maboma katika nchi ya Yuda. Kisha akaiondoa miungu migeni pamoja na kile kinyago Nyumbani mwa Bwana, nazo meza zote za kutambikia, alizozijenga milimani penye Nyumba ya Bwana namo Yerusalemu, akazitupa huko nje ya mji. Akaitengeneza tena meza ya kumtambikia Bwana, akachoma juu yake ng'ombe za tambiko za kushukuru na za kusifu, nao Wayuda akawaagiza kumtumikia Bwana Mungu wa Isiraeli. Lakini watu hawakuacha kutambika vilimani, lakini huko nako siku zile wakamtambikia Bwana Mungu wao tu. Mambo mengine ya Manase na maombo yake, aliyomwomba Mungu wake, na mambo ya wachunguzaji waliosema naye katika Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli tunayaona, yametiwa katika mambo ya wafalme wa Waisiraeli. Maombo yake na vilio vyake na makosa yake yote ya kuvunja maagano na mahali, alipojenga vijumba vya kutambikia vilimani, napo aliposimamisha miti ya Ashera na vinyago vingine, alipokuwa hajajinyenyekeza bado, yote yamekwisha kuandikwa katika mambo ya wachunguzaji. Kisha Manase akaja kulala na baba zake, wakamzika nyumbani mwake, naye mwanawe Amoni akawa mfalme mahali pake. Amoni alikuwa mwenye miaka 22 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 2 mle Yerusalemu. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, kama baba yake Manase alivyofanya, navyo vinyago vyote, baba yake Manase alivyovitengeneza, Amoni akavitambikia na kuvitumikia. Hakujinyenyekeza mbele ya Bwana, kama baba yake Manase alivyojinyenyekeza, kwani yeye Amoni alikora manza nyingi. Ndipo, watumishi wake walipomlia njama, wakamwua nyumbani mwake. Lakini watu wa nchi hiyo wakawaua wote waliomlia mfalme Amoni njama, kisha hao watu wa nchi hiyo wakamfanya mwanawe Yosia kuwa mfalme mahali pake. Yosia alikuwa mwenye miaka 8 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 31 mle Yerusalemu. Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana, akaendelea na kuzishika njia za baba yake Dawidi, hakuziacha na kujiendea kuumeni wala kushotoni. Katika mwaka wa nane wa ufalme wake, yeye alipokuwa akingali mvulana, alianza kumtafuta Mungu wa baba yake Dawidi; tena katika mwaka wa kumi na mbili alianza kuitakasa nchi ya Yuda na mji wa Yerusalemu na kuyaondoa matambiko ya vilimani na miti ya Ashera na vinyago vingine vya kuchonga navyo vilivyoyeyushwa. Usoni pake wakazivunjavunja meza za kuyatambikia Mabaali, nayo mifano ya jua iliyosimamishwa juu yao wakaikatakata, nayo miti ya Ashera na vinyago vingine vya kuchonga navyo vilivyoyeyushwa akavipondaponda, hata vikawa mavumbi, kisha hayo mavumbi akayamwaga juu ya makaburi yao waliovitambikia. Nayo mifupa ya watambikaji wao akaiteketeza juu ya meza zao za kutambikia. Ndivyo, alivyoitakasa nchi ya Yuda na mji wa Yerusalemu. Namo mijini mwa Manase na mwa Efuraimu, hata mwa Nafutali katika mahame yao yaliyokuwapo po pote ndimo, alimozivunjavunja meza za kutambikia, akaiponda miti ya Ashera navyo vinyago vingine, hata vikawa mavumbi, nayo mifano yote ya jua akaikatakata katika nchi yote ya Isiraeli, kisha akarudi Yerusalemu. Katika mwaka wa kumi na nane wa ufalme wake alipokwisha kuitakasa nchi na Nyumba hiyo, akamtuma Safani, mwana wa Asalia, na Masea, mkuu wa mji, na Yoa, mwana wa Yoahazi, aliyekuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa, kwenda kuitengeneza vizuri Nyumba ya Bwana Mungu wake. Wakaja kwa mtambikaji mkuu Hilkia, wakampa zile fedha zilizopelekwa Nyumbani mwa Mungu, ambazo wangoja vizingiti walizikusanya kwao Wamanase na Waefuraimu na kwa Waisiraeli wote wengine na kwa Wayuda na Wabenyamini wote, hata kwa wenyeji wa Yerusalemu. Wakazitia hizo fedha mikononi mwao wenye hiyo kazi waliowekwa kuzisimamia kazi za Nyumbani mwa Bwana; nao wenye hiyo kazi wakazipa wao waliozifanya kazi Nyumbani mwa Bwana za kuirudishia upya Nyumba ya Bwana kwa kuitengeneza vizuri. Nao wakazipa maseremala na waashi za kununua mawe ya kuchonga na miti ifaayo ya kuungia na ya boriti za vipaa vya nyumba. Watu hao walifanya kazi zao kwa welekevu; waliowekwa kuwasimamia katika kazi ni Walawi Yahati na Obadia waliokuwa wa mlango wa Merari, tena Zakaria na Mesulamu waliokuwa wa mlango wa Kehati. Nao walawi wote waliojua kupiga vyombo vya kuimbia walikuwa kwao wachukuzi, nao wakawasimamia wafanya kazi wote, kila mmoja katika utumishi wake, tena walikuwako Walawi walio waandishi na wenye amri na walinda malango. Walipozitoa zile fedha zilizopelekwa Nyumbani mwa Bwana, ndipo, mtambikaji Hilkia alipokiona kitabu cha Maonyo ya Bwana, aliyopewa Mose. Hilkia akasema na kumwambia mwandishi Safani: Nimeona Kitabu cha Maonyo Nyumbani mwa Bwana! Kisha Hilkia akampa Safani hicho kitabu. Safani akakipeleka hicho kitabu kwa mfalme, tena akampasha mfalme habari kwamba: Yote yaliyowekwa mikononi mwa watumishi wako, wao wanayafanya. Fedha zilizooneka Nyumbani mwa Bwana wamezimimina, wakawapa wasimamizi mikononi mwao namo mikononi mwao wafanya kazi. Kisha mwandishi Safani akamsimulia mfalme kwamba: Mtambikaji Hilkia amenipa kitabu; kisha Safani akasoma humo mbele ya mfalme. Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya Maonyo, akayararua mavazi yake. Kisha mfalme akamwagiza Hilkia na Ahikamu, mwana wa Safani, na Abudoni, mwana wa Mika, na mwandishi Safani na Asaya aliyekuwa mtumishi wa mfalme kwamba: Nendeni kuniulizia Bwana mimi na masao ya Waisiraeli na ya Wayuda kwa ajili ya maneno ya hiki kitabu kilichooneka, kwani makali ya Bwana yenye moto ni makuu, nayo humwagika kwetu, kwa kuwa baba zetu hawakulishika Neno la Bwana na kuyafanya yote yaliyoandikwa humu kitabuni. Ndipo, Hilkia alipokwenda pamoja nao wa mfalme kwa mfumbuaji wa kike Hulda, mkewe Salumu, mwana wa Tokati, mwana wa Hasira aliyeyaangalia mavazi; naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili, wakamwambia maneno yaleyale. Akawaambia: Ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mwambieni yule mtu aliyewatuma kwangu: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikileta mabaya mahali hapa, yawapate wenyeji wa hapa, ndio viapo vyote vilivyoandikwa katika kitabu, walichokisoma masikioni pa mfalme wa Wayuda, kwa kuwa wameniacha, wakavukizia miungu mingine, wanikasirishe kwa matendo yote ya mikono yao; kwa hiyo makali yangu yenye moto yatamwagwa hapa, wala hayatazimika. Naye mfalme wa Wayuda aliyewatuma kumwuliza Bwana mwambieni haya: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Kwa kuwa hapo, ulipoyasikia maneno yale, moyo wako umelegea, ukajinyenyekeza mbele ya Mungu papo hapo ulipoyasikia maneno yake, aliyoyasema ya mahali hapa na ya wenyeji wake, ukajinyenyekeza kweli mbele yangu na kuyararua mavazi yako na kunililia mimi, basi, kwa hiyo mimi nami nimekusikia; ndivyo, asemavyo Bwana. Utaniona, nikikuita, uje kukutana na baba zako; ndipo, utakapopelekwa kulala kaburini mwako na kutengemana, macho yako yasiyaone hayo mabaya yote, nitakayopaletea mahali hapa na wenyeji wa hapa. Kisha wakampelekea mfalme majibu haya. Ndipo, mfalme alipotuma wajumbe, akawakusanya wazee wote wa Wayuda na wa Yerusalemu. Kisha mfalme akapanda kwenda Nyumbani mwa Bwana pamoja na Wayuda wote na wenyeji wa Yerusalemu na watambikaji na Walawi na watu wote pia, wakubwa kwa wadogo, akawasomea masikioni pao maneno yote ya kitabu cha Agano kilichooneka Nyumbani mwa Bwana. Kisha mfalme akaja kusimama katika ulingo wake, akafanya mbele ya Bwana agano la kumfuata Bwana na kuyaangalia maagizo yake na mashuhuda yake na maongozi yake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, ayafanye maneno ya Agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Nao wote walioonekana mle Yerusalemu namo katika nchi ya Benyamini akawashurutisha kulisimamia hilo agano, nao wenyeji wa Yerusalemu wakafanya, kama Agano la Mungu aliye Mungu wa baba zao lilivyowatakia. Kisha Yosia akaondoa kabisa matambikoi yote yatapishayo katika nchi zote zilizokuwa zao wana wa Isiraeli, nao watu wote walioonekana kwa Waisiraeli akawashurutisha kumtumikia Bwana Mungu wao, nazo siku zake zote za kuwapo hawakuacha kumfuata Bwana Mungu wa baba zao. Kisha Yosia akamfanyia Bwana huko Yerusalemu sikukuu ya Pasaka, wakachinja wana kondoo wa Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Akawaagiza watambikaji kuja kuzifanya kazi zao ziwapasazo, akawashikiza mioyo, watumikie Nyumbani mwa Bwana. Akawaambia Walawi waliowafundisha Waisiraeli wote, waliokuwa watakatifu wa Bwana: Liwekeni Sanduku takatifu katika hiyo Nyumba, aliyoijenga Salomo, mwana wa Dawidi, mfalme wa Waisiraeli! Msilichukue tena mabegani! Sasa mtumikieni Bwana Mungu wenu, mwatumikie nao walio ukoo wake, mkijiweka tayari kwa milango ya baba zenu na kwa zamu zenu, kama Dawidi, mfalme wa Isiraeli, alivyoviandika, na kama mwanawe Salomo alivyoviandika naye. Simameni Patakatifu kwa vyama vya milango ya baba vya ndugu zenu walio watuwatu tu, kila fungu la mlango mmoja lipate Walawi. Kisha wachinjeni wana kondoo wa Pasaka na kujitakasa, kuwatengenezeeni ndugu zenu na kufanya, kama Bwana alivyoagiza kinywani mwa Mose! Kisha mfalme akawatolea watu kondoo na wana mbuzi, wote kuwa wa Pasaka wa watu wote waliooneka, wote wakawa 30000 na ng'ombe 3000, wote walitoka katika makundi ya mfalme. Nao wakuu wake waliwatolea watu na watambikaji na Walawi vipaji kwa kupenda wenyewe: Hilkia na Zakaria na Yehieli waliokuwa wenye amri Nyumbani mwa Mungu waliwapa watambikaji wana kondoo wa Pasaka 2600 na ng'ombe 300. Nao wakuu wa Walawi Konania na ndugu zake Semaya na Netaneli, tena Hasabia na Yieli na Yozabadi waliwatolea Walawi kondoo wa Pasaka 5000 na ng'ombe 500. Utumishi ulipokwisha kutengenezwa, watambikaji wakaja kusimama mahali pao, nao Walawi kwa zamu zao, kama mfalme alivyoagiza. Walipowachinja wana kondoo wa Pasaka, watambikaji wakazipokea damu mikononi mwao wakazinyunyiza, nao Walawi wakawa wakichuna. Wakaziondoa nyama za kuchoma na kuvipa vyama vya milango yao walio watuwatu tu, wenyewe wamtolee Bwana, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Mose. Nao ng'ombe wakawafanya vivyo hivyo. Kisha nyama za Pasaka wakazioka motoni, kama walivyoagizwa; lakini zile za vipaji vitakatifu wakazipika katika vyungu na katika masufuria na katika makaango, wakazipelekea upesi wale walio watuwatu tu. Kisha wakajiandalia wenyewe na watambikaji, kwani watambikaji, wana wa Haroni, walifanya kazi za kuziteketeza ng'ombe za tambiko pamoja na mafuta mpaka usiku. Kwa hiyo Walawi wakajiandalia wenyewe na watambikaji, wana wa Haroni. Nao waimbaji, wana wa Asafu, walisimama mahali pao, kama Dawidi na Asafu na Hemani na Yedutuni, mchunguzaji wa mfalme, walivyoviagiza; nao walinda malango walisimama kila penye lango lake, hawakuwa na shuruti kuondoka katika utumishi wao, kwani ndugu zao Walawi waliwaandalia. Ndivyo, kazi zote za utumishi wa Bwana zilivyotengenezwa siku ile ya kufanya Pasaka pamoja na kuteketeza ng'ombe za tambiko mezani pa kumtambikia Bwana, kama mfalme Yosia alivyoagiza. Nao wana wa Isiraeli waliokuwako wakafanya Pasaka siku hiyo, nayo hiyo sikukuu ya Mikate isiyochachwa wakaila siku saba. Pasaka kama hii haikufanywa kwa Waisiraeli tangu siku za mfumbuaji Samweli; wafalme wote wa Waisiraeli hawakufanya Pasaka, kama Yosia alivyoifanya pamoja na watambikaji na Walawi na Wayuda na Waisiraeli wote waliokuwako na wenyeji wa Yerusalemu. Pasaka hii ikafanywa katika mwaka wa kumi na nane wa ufalme wa Yosia. Hayo yote, aliyoyafanya ya kuitengeneza Nyumba hiyo, yalipokwisha kufanyika, akapanda Neko, mfalme wa Misri, kwenda kupigana Karkemisi penye jito la Furati, naye Yosia akatoka kumpinga. Yule akatuma wajumbe kwake kumwambia: Tuko na neno gani mimi na wewe, mfalme wa Yuda? Leo sikukujia wewe, ila ule mlango ninaotaka kupigana nao. Naye Mungu ameniagiza kwenda upesi; jiepushe kwake Mungu aliye upande wangu, asije kukuangamiza! Lakini Yosia hakuugeuza uso wake na kumwacha, ila alijipa moyo mwingine kwenda kupigana naye, asiyasikie maneno ya Neko yaliyotoka kinywani mwa Mungu, akaenda kupigana naye bondeni kwa Megido. Wenye kupiga mishale wakampiga mfalme Yosia; ndipo, mfalme alipowaambia watumishi wake: Nipitisheni huku! Kwani nimeumia sana. Ndipo, watumishi wake walipomtoa katika gari na kumweka katika gari la pili, alilokuwa nalo, wakampeleka Yerusalemu; ndiko, alikokufa. Wakamzika makaburini kwa baba zake. Nao Wayuda na Wayerusalemu wote wakamlilia Yosia, naye Yeremia akamwombolezea Yosia. Nao waimbaji wote waume na wake humtaja Yosia katika maombolezo yao hata siku hii ya leo; hivi vikawa desturi kwao Waisiraeli, nayo yamekwisha kuandikwa katika maombolezo. Mambo mengine ya Yosia na matendo ya upole wake yaliyopatana nayo yaliyoandikwa katika Maonyo ya Bwana, nayo mambo yake ya kwanza na ya mwisho tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Waisiraeli na wa Wayuda. Watu wa nchi hii wakamchukua Yoahazi, mwana wa Yosia, wakamfanya kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia mle Yerusalemu. Yoahazi alikuwa mwenye miaka 23 alipoupata ufalme, akawa mfalme miezi 3 mle Yerusalemu; ndipo, mfalme wa Misri alipomwondoa Yerusalemu, akailipisha nchi hii vipande 100 vya fedha, ndio shilingi milioni na 200000, na kipande kimoja cha dhahabu, ndio shilingi 220000. Mfalme wa Misri akamfanya ndugu yake Eliakimu kuwa mfalme wa Wayuda na wa Wayerusalemu, akaligeuza jina lake, akamwita Yoyakimu; lakini ndugu yake Yoahazi Neko akamchukua, akampeleka Misri. Yoyakimu alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 11 mle Yerusalemu, akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana Mungu wake. Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, akamjia, akamfunga kwa minyororo kumpeleka Babeli. Navyo vyombo vingine vya Nyumba ya Bwana Nebukadinesari akavipeleka Babeli, akvitia jumbani mwake huko Babeli. Mambo mengine ya Yoyakimu na matapisho yake, aliyoyafanya, na mengine yaliyooneka kwake tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Waisiraeli na wa Wayuda. Naye mwanawe Yoyakini akawa mfalme mahali pake. Yoyakini alikuwa mwenye miaka 8 alipoupata ufalme, akawa mfalme miezi mitatu na siku kumi mle Yerusalemu, akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana. Mwaka mwingine ulipoanza, mfalme Nebukadinesari akatuma, akampeleka Babeli pamoja na vyombo vya Nyumba ya Bwana, alivyovitamani, akamfanya ndugu yake Sedekia kuwa mfalme wao Wayuda na Wayerusalemu. Sedekia alikuwa mwenye miaka 21 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 11 mle Yerusalemu. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana Mungu wake; hakujinyenyekeza mbele ya mfumbuaji Yeremia aliyekuwa kinywa cha Bwana. Hata mfalme Nebukadinesari akamkataa akiacha kumtii, naye alikuwa amemwapisha na kumtaja Mungu, akaushupaza ukosi wake, nao moyo wake akaufanya kuwa mgumu, asirudi kwake Bwana Mungu wa Isiraeli. Nao wakuu wote wa watambikaji na wa watu wakazidi kuyavunja maagano na kufanya mengi kama hayo matapisho yote ya wamizimu, hata Nyumba ya Bwana wakaichafua, aliyoitakasa mle Yerusalemu. Yeye Bwana Mungu wa baba zao akatuma kwao wajumbe pasipo kuchoka kuwatumia, kwani aliwaonea walio ukoo wake huruma, hata Kao lake. Lakini wao wakawasimanga wajumbe wa Mungu, nayo maneno yake wakayabeza na kuwafyoza wafumbuaji wake, mpaka makali ya Bwana yawakayo moto wa kuwakasirikia walio ukoo wake yakamkwea, asipatikane aliyeweza kuwaponya. Ndipo, alipomhimiza mfalme wa Wakasidi kupanda kwenda kwao, akawaua vijana wao kwa panga katika Nyumba iliyokuwa Patakatifu pao, hakuwahurumia, wala mvulana wala mwanamwali, wala wazee wala wakongwe, wote pia Mungu aliwatia mkononi mwake. Navyo vyombo vyote vya Nyumbani mwa Mungu, vikubwa kwa vidogo, navyo vilimbiko vya Nyumbani mwa Bwana, navyo vilimbiko vya mfalme na vya wakuu wake, vyote pia akavipeleka Babeli. Kisha wakaiteketeza Nyumba ya Mungu wakazibomoa kuta za boma la Yerusalemu, nayo majumba mazuri yote wakayateketeza kwa moto, navyo vyombo vyote vyenye kima wakaviangamiza. Nao wote waliosalia, wasiouawa na panga, akawahamisha kwenda Babeli, wakawa watumwa wake yeye na wa wanawe, mpaka Wapersia walipopata ufalme. Ndivyo, lilivyotimia neno la Bwana, alilolisema kinywani mwa Yeremia, nchi hii ipate kuimaliza miaka yake ya mapumziko; kwani siku zote za kukaa peke yake tu ilipumzika, hata ikatimia miaka 70. Katika mwaka wa kwanza wa Kiro, mfalme wa Wapersia, ndipo, lilipotimia neno la Bwana, alilolisema kinywani mwa Yeremia, maana Bwana akaiamsha roho yake Kiro, mfalme wa Wapersia, akatangaza mbiu katika ufalme wake wote kwa vinywa vya watu na kwa barua kwamba: Hivi ndivyo, anavyosema Kiro, mfalme wa Wapersia: Ufalme wote wa nchi hii amenipa Bwana Mungu wa mbinguni, naye mwenyewe akaniagiza kumjengea Nyumba kule Yerusalemu katika nchi ya Yuda; ye yote wa kwenu aliye wa ukoo wake na apande kurudi kwao, naye Bwana Mungu wake awe naye! Katika mwaka wa kwanza wa Kiro, mfalme wa Wapersia, ndipo, lilipotimia neno la Bwana, alilolisema kinywani mwa Yeremia, maana Bwana akaiamsha roho yake Kiro, mfalme wa Wapersia, akatangaza mbiu katika ufalme wake wote kwa vinywa vya watu na kwa barua kwamba: Hivi ndivyo, anavyosema Kiro, mfalme wa Wapersia: Ufalme wote wa nchi hii amenipa Bwana Mungu wa mbinguni, naye mwenyewe akaniagiza kumjengea Nyumba kule Yerusalemu katika nchi ya Yuda. Ye yote wa kwenu aliye wa ukoo wake Mungu wake awe naye, na apande kwenda Yerusalemu katika nchi ya Yuda kuijenga Nyumba ya Bwana Mungu wa Isiraeli. Yeye akaaye Yerusalemu ni Mungu. Tena kila atakayesalia mahali po pote, anapokaa ugenini, watu wa mahali pale sharti wamsaidie kwa kumpa fedha na dhahabu na vyombo na nyama wa kufuga pamoja na vipaji vingine, wanavyovitaka wenyewe vya kuitolea Nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu. Ndipo, wao waliokuwa vichwa vya milango ya Yuda na ya Benyamini pamoja na watambikaji na Walawi walioamshwa roho zao na Mungu wakaondoka kwenda kuijenga Nyumba ya Bwana iliyoko Yerusalemu. Nao waliokaa na kuwazunguka wakaitia mikono yao nguvu kwa kuwapa fedha na dhahabu na vyombo na nyama wa kufuga na vitu vyenye kima, tena vipaji vyote, walivyovitoa wenyewe vya tambiko. Naye mfalme Kiro akavitoa vyombo vyote vya Nyumba ya Bwana, Nebukadinesari alivyovitoa Yerusalemu na kuvitia jumbani mwake. Hivyo Kiro, mfalme wa Wapersia, akavitoa na kuvitia mikononi mwa mtunza malimbiko Mitiridati, naye akavihesabu alipompa Sesebasari, mkuu wa Wayuda. Hii ndiyo hesabu yao: sinia za dhahabu 30, sinia za fedha 1000, visu 29; vinyweo vya dhahabu 30, vinyweo vya fedha vya namna ya pili 410, vyombo vingine 1000. Vyombo vyote vya dhahabu na vya fedha vilikuwa 5400. Hivi vyote Sesebasari alikwenda navyo, wale waliotekwa na kuhamishwa walipotoka Babeli kwenda kupanda Yerusalemu. Hawa ndio wana wa lile jimbo waliotoka katika kifungo cha kuhamishwa, aliowateka Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, na kuwahamisha kwenda Babeli, wakapanda kurudi Yerusalemu na Yuda, kile mtu mjini kwake. Waliokuja na Zerubabeli ndio: Yesua, Nehemia, Seraya, Relaya, Mordekai, Bilsani, Misipari, Bigwai, Rehumu, Baana. Hesabu ya waume wa ukoo wa Isiraeli ni hii: wana wa Parosi 2172; wana wa Sefatia 372; wana wa Ara 775; wana wa Pahati-Moabu, ndio wana wa Yesua na wa Yoabu 2812; wana wa Elamu 1254; wana wa Zatu 945; wana wa Zakai 760; wana wa Bani 642; wana wa Bebai 623; wana wa Azgadi 1222; wana wa Adonikamu 666; wana wa Bigwai 2056; wana wa Adini 454; wana wa Ateri walio wa Hizikia 98; wana wa Besai 323; wana wa Yora 112; wana wa Hasumu 223; wana wa Gibari 95; wana wa Beti-Lehemu 123; waume wa Netofa 56; waume wa Anatoti 128; wana wa Azimaweti 42; wana wa Kiriati-Arimu, wa Kefira na wa Beroti 743; wana wa Rama na wa Geba 621; waume wa Mikimasi 122; waume wa Beteli na wa Ai 223; wana wa Nebo 52; wana wa Magibisi 156; wana wa Elamu wa pili 1254; wana wa Harimu 320; wana wa Lodi na wa Hadidi na wa Ono 725; wana wa Yeriko 345; wana wa Senaa 3630. Watambikaji walikuwa hawa: wana wa Yedaya wa mlango wa Yesua 973; wana wa Imeri 1052; wana wa Pashuri 1247; wana wa Harimu 1017. Walawi walikuwa hawa: wana wa Yesua na wa Kadimieli walio wa wana wa Hodawia 74. Waimbaji walikuwa wana wa Asafu 128. Wana wa walinda malango walikuwa wana wa Salumu, wana wa Ateri, wana wa Talmoni, wana wa Akubu, wana wa Hatita, wana wa Sobai, wote pamoja walikuwa 139. Watumishi wa Nyumbani mwa Mungu walikuwa hawa: wana wa Siha, wana wa Hasufa, wana wa Tabaoti, wana wa Kerosi, wana wa Siaha, wana wa Padoni, wana wa Lebana, wana wa Hagaba, wana wa Akubu wana wa Hagabu, wana wa Samulai, wana wa Hanani, wana wa Gideli, wana wa Gahari, wana wa Raya, wana wa Resini, wana wa Nekoda, wana wa Gezamu, wana wa Uza, wana wa Pasea, wana wa Besai, wana wa Asina, wana wa Munimu, wana wa Nefisimu, wana wa Bakibuki, wana wa Hakufa, wana wa Harihuri, wana wa Basiluti, wana wa Mehida, wana wa Harsa, wana wa Barkosi, wana wa Sisera, wana wa Tema, wana wa Nesia na wana wa Hatifa. Wana wa watumwa wa Salomo walikuwa hawa: wana wa Sotai, wana wa Sofereti, wana wa Peruda, wana wa Yala, wana wa Darkoni, wana wa Gideli, wana wa Sefatia, wana wa Hatili, wana wa Pokereti-Hasebaimu, wana wa Ami. Watumishi wa Nyumbani mwa Mungu na wana wa watumwa wa salomo wote pamoja walikuwa 392. Nao hawa ndio waliopanda toka Teli-Mela na Teli-Harsa na Kerubu-Adani na Imeri, lakini hawakuweza kuijulisha milango ya baba zao, wala vizazi vyao, kama ndio Waisiraeli: wana wa Delaya, wana wa Tobia, wana wa Nekoda; nao walikuwa watu 652. Tena kwao watambikaji: wana wa Habaya, wana wa Hakosi, wana wa Barzilai aliyechukua mmoja wao binti Barzilai wa Gileadi, awe mkewe, kwa hiyo aliitwa kwa jina lao. Hawa walikitafuta kitabu chao cha udugu wao, lakini hawakukiona, kwa hiyo wakakatazwa utambikaji. Mtawala nchi akawaambia: Msile kabisa vyakula vitokavyo Patakatifu Penyewe, mpaka atakapoondokea mtambikaji mwenye Urimu na Tumimu (Mwanga na Kweli). Huo mkutano wote pamoja walikuwa watu 42360, pasipo watumwa na vijakazi wao, nao walikuwa 7337; tena walikuwako waimbaji wa kiume na wa kike 200. Farasi wao walikuwa 736, nyumbu wao 245, ngamia wao 435, tena punda 6720. Walipofika penye Nyumba ya Bwana iliyokuwamo Yerusalemu, ndipo, wakuu wa milango walipoitolea wenyewe Nyumba ya Mungu vipaji vya kuijengea tena mahali hapo, ilipokuwa. Kwa hiyo, walivyoweza, wakatoa vipaji vyao, wakavitia katika kilimbiko cha jengo: vipande vya dhahabu vilivyoitwa Dariko 61000, ndio shilingi kama milioni mbili na 440000 na vipande vya fedha vilivyoitwa Mane 5000, ndio shilingi kama milioni, na mavazi ya watambikaji 100. Kisha watambikaji na Walawi, nao watu wengine na waimbaji na walinda malango nao watumishi wa Nyumbani mwa Mungu wakakaa katika miji yao, nao Waisiraeli wote wakakaa katika miji yao. Mwezi wa saba ulipofika, wana wa Isiraeli wakikaa mijini mwao, ndipo, watu walipokusanyika Yerusalemu kama mtu mmoja. Akaondokea Yesua, mwana wa Yosadaki, pamoja na ndugu zake waliokuwa watambikaji na Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na ndugu zake, wakaijenga meza ya kumtambikia Mungu wa Isiraeli, wapate kuteketeza juu yake ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, kama ilivyoandikwa katika Maonyo ya Mose aliyekuwa mtu wa Mungu. Wakaiweka hiyo meza ya kutambikia hapo penye misingi yake. Kwa kushikwa na woga wa wenyeji wa hiyo nchi, wakamtolea Bwana hapo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, hizo ng'ombe za tambiko wakazitoa za asubuhi na za jioni. Kisha wakala sikukuu ya Vibanda, kama ilivyoandikwa; wakazitoa ng'ombe za tambiko za kila siku kwa hesabu iliyowekwa ya ng'ombe za tambiko zipasazo kila siku moja. Baadaye makaitoa nayo ng'ombe ya tambiko isiyokoma kutolewa ya kila siku, nazo za miandamo ya mwezi, nazo za sikukuu zote za Bwana zilizowekwa kuwa takatifu, nazo za kila mtu aliyetaka mwenyewe kumtolea Bwana kipaji cha tambiko. Siku ya kwanza ya mwezi wa saba ndiyo, waliyoanzia kumtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, lakini Jumba la Bwana lilikuwa halijawekewa misingi. Kisha wakachanga fedha za kuwapa mafundi wa kuchonga mawe na miti, nao Wasidoni na Watiro wakawapa vilaji na vinywaji na mafuta, walete miti ya miangati toka kwao Libanoni wakiipitisha baharini hata Yafo, kwani Kiro, mfalme wa Wapersia, aliwapa ruhusa. Katika mwaka wa 2 wa kuja kwao penye Nyumba ya Mungu huko Yerusalemu katika mwezi wa pili ndipo, Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na Yesua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zao wengine walipoanza kazi za kuijenga pamoja na watambikaji na Walawi nao wote waliorudi Yerusalemu wakitoka kwenye kutekwa; wakaweka Walawi waliokuwa wa miaka ishirini na zaidi kuwa wasimamizi wa kuziangalia hizo kazi za Nyumba ya Bwana. Yesua na wanawe na ndugu zake na Kadimieli na wanawe waliokuwa wana wa Yuda wakasimama kama mtu mmoja wakiwaangalia watu wa kazi pale penye Nyumba ya Mungu. Vilevile wana wa Henadadi na wana wao na ndugu zao waliokuwa Walawi. Waashi walipoanza kuyapigilia mawe ya misingi ya Jumba la Bwana wakaweka hapo watambikaji waliovikwa mavazi yao, wakishika matarumbeta, nao Walawi waliokuwa wana wa Asafu, wakishika matoazi, wamtukuze Bwana na kumwimbia wimbo wa Dawidi, mfalme wa Isiraeli. Wakaitikiana na kumtukuza na kumshukuru Bwana kwamba: Bwana ni mwema, upole wake ni wa kale na kale, nao huwakalia Waisiraeli. Nao watu wote pia wakapaza sana sauti za kupiga shangwe, wamtukuze Bwana, kwa kuwa misingi ya Nyumba ya Bwana iliwekwa. Lakini wengi wao watambikaji na Walawi nao waliokuwa vichwa vya milango, ndio wazee walioiona Nyumba ya kwanza wakalia machozi kwa sauti kuu, misingi ya Nyumba hii ilipowekwa machoni pao, lakini wengine wengi wakazipaza sauti zao za kupiga shangwe na kelele za furaha. Lakini watu hawakuweza kuzipambanua sauti za shangwe zenye furaha nazo sauti za vilio vya wale watu, kwani watu walizidisha sana kuzipaza sauti zao za shangwe; hizo sauti zikasikilika hata mbali. Wapingani wao Wayuda na Wabenyamini waliposikia, ya kuwa waliorudi kwenye kutekwa wanamjengea Bwana Mungu wa Isiraeli Jumba, ndipo, walipomkaribia Zerubabeli nao waliokuwa vichwa vya milango, wakawaambia: Na tujenge pamoja nanyi! Kwani nasi tunamtumikia Mungu wenu kama ninyi, tunamtambikia tangu hapo, Esari-Hadoni, mfalme wa Asuri, alipotuleta huku, tukae. Lakini Zerubabeli na Yesua nao wenzao wengine waliokuwa vichwa vya milango ya Isiraeli wakawaambia: Haipasi, ninyi na sisi tumjengee Mungu wetu Nyumba pamoja, ila sisi tunataka kumjengea Bwana Mungu wa Isiraeli Nyumba peke yetu, kama mfalme Kiro, mfalme wa Wapersia, alivyotuagiza. Ndipo, wenyeji wa hiyo nchi walipoilegeza mikono ya Wayuda na kuwatia woga, wasiendelee kujenga. Wakawapenyezea viongozi fedha, walivunje hilo hauri lao, siku zote Kiro alipokuwa mfalme wa Wapersia, mpaka Dario alipoupata ufalme kuwa mfalme wa Wapersia. Ahaswerosi alipoupata ufalme, katika siku za mwanzo wa ufalme wake wakaandika barua ya kuwashtaki waliokaa Yuda na Yerusalemu. Siku za Artasasta Bisilamu na Mitiridati na Tabeli na wenziwe wengine wakaandika barua kwa Artasasta, mfalme wa Wapersia; nayo maandiko ya barua hii yalikuwa yameandikwa Kishami, nayo maneno yake yalikuwa yamegeuzwa kuwa ya Kishami vilevile: Mwenye amri Rehumu na mwandishi Simusai waliandika barua moja kwa mfalme Artasasta kwa ajili ya Yerusalemu ya kwamba: Kale mwenye amri Rehumu na mwandishi Simusai na wenzao wengine waliandika barua, wao pamoja na Wadinai na Waafarsatiki, tena Watarpeli, Waafarsi, Waarkewi, Wababeli, Wasusaniki, Wadehai, Waelamu na makabila mengine, Osinapari aliyekuwa mwenye ukuu na utukufu aliowateka na kuwahamisha akiwakalisha katika miji ya Samaria na katika miji mingine iliyoko ng'ambo hii ya jito kubwa na penginepengine; basi, huu ndio mwandiko wa pili wa barua yao, waliyoituma kwake: Kwa mfalme Artasasta watumwa wako tunaokaa ng'ambo ya huku ya jito kubwa na penginepengine: Na ijulike kwa mfalme, ya kuwa Wayuda waliotoka kwako wapande kufika kwetu Yerusalemu, wanaujenga mji huu mbaya wenye ukatavu, boma lake wamelimaliza, nayo misingi yake wameitengeneza. Tena na ijulike kwa mfalme, ya kuwa mji huu ukijengwa, boma lake likimalizwa, watu wake hawatatoa kodi wala ushuru wa forodhani wala wa njiani, mwisho wafalme watapungukiwa fedha zao. Kwa kuwa tunakula chumvi ya jumba la mfalme, haitupasi kutazama tu, mfalme akiharibiwa mali zake, kwa hiyo tumetuma kumjulisha mfalme mambo haya. Sasa na wachunguze katika kitabu cha makumbusho ya baba zako. Ndipo, utakapoyaona humo kitabuni mwenye makumbusho, utajua, ya kuwa mji huu ni mji wenye ukatavu uliowaharibia wafalme nchi hata mali zao, hata mafujo wameyafanya kwao tangu siku za kale. Kwa sababu hii mji huo ukabomolewa. Sisi tunamjulisha mfalme, ya kwamba: Mji huu ukijengwa, nalo boma lake likimalizwa, basi, kwa hiyo hutakaa nalo hilo fungu la nchi lililoko ng'ambo ya huku ya jito kubwa. Ndipo, mfalme alipotuma jibu kwa mwenye amri Rehumu na kwa mwandishi Simusai na kwa wenzao wengine waliokaa Samaria na penginepo ng'ambo ya huko ya jito kubwa kwamba: Salamu na mengine yafuatayo! Barua, mliyoituma kwetu, imesomwa masikioni pangu neno kwa neno. Nami nikatoa amri, wayachunguze hayo; ndipo, walipoona, ya kuwa mji huo uliwainukia wafalme tangu siku za kale, hata mivurugo na mafujo yalifanyika humo. Nao Wafalme wenye nguvu walikuwamo Yerusalemu, wakazitawala nchi zote zilizoko ng'ambo ya huko ya jito kubwa, wakapewa kodi na ushuru wa forodhani na wa njiani. Kwa hiyo toeni amri ya kuwakataza watu hao, mji huo usijengwe, hata amri itakapotolewa na mimi. Nanyi mwangalie, msipoteze njia ya kulitengeneza jambo hili, wafalme wasipatwe na hasara kubwa wakipunguziwa mali zao! Papo hapo mwandiko wa pili wa barua ya mfalme Artasasta uliposomwa masikioni pao Rehumu na mwandishi Simusai na wenzao, ndipo, walipopiga mbio kwenda Yerusalemu kwa wayuda, wakawakataza majengo kwa ukorofi na nguvu. Hapo ndipo, zilipokoma kazi za Nyumba ya Bwana mle Yerusalemu, zikawa zimekoma mpaka mwaka wa pili wa ufalme wa Dario, mfalme wa Wapersia. Ndipo, wafumbuaji Hagai na Zakaria, mwana wa Ido, waliokuwa wafumbuaji, walipowafumbulia Wayuda waliokaa Yuda na Yerusalemu mambo hayo katika Jina la Mungu wa Isiraeli aliyewajia. Ndipo, Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na Yesua, mwana wa Yosadaki, walipoondokea, wakaanza tena kuijenga Nyumba ya Mungu mle Yerusalemu, nao wafumbuaji wa Mungu wakawa nao wakiwashikiza. Siku hizo wakawajia Tatinai, mtawala nchi zilizoko ng'ambo ya huku ya jito kubwa, na Setari-Bozinai pamoja na wenzao, wakawauliza: Ni nani aliyewatolea amri ya kuijenga nyumba hii na kuzimaliza kuta hizi? Ndipo, tulipowaambia hayo majina ya watu waliolijenga jengo hili. Lakini jicho la Mungu wao lilikuwa limewaelekea wazee wa Wayuda, wao wasiwakataze kujenga, mpaka amri ya Dario ifike, wapate barua kwa ajili ya jambo hili. Mwandiko wa pili wa barua, waliyoituma kwa mfalme Dario akina Tatinai, mtawala nchi zilizoko upande wa huku wa jito kubwa, na Setari-Bozinai na wenzake Waafarsaki waliokaa upande wa huku wa jito kubwa. Katika barua hiyo, waliyoituma kwake, yalikuwa yameandikwa haya: Salamu zote kwa mfalme Dario! Na ijulikane kwa mfalme, ya kuwa tumekwenda katika nchi ya Yuda mle mjini, Nyumba ya Mungu mkuu ilimo, nayo inajengwa kwa mawe makubwa ya kuchonga, nazo kuta zake zinapigiliwa mbao. Kazi hizi zinafanywa kwa bidii, zinaendelea vizuri kwa nguvu za mikono yao. Ndipo, tulipowauliza wazee wale na kuwaambia haya: Ni nani aliyewaagiza kuijenga nyumba hii na kuzimaliza hizi kuta? Tukawauliza nayo majina yao, tukujulishe; yakaandikwa majina yao walio vichwa vyao. Nazo hizi ndizo habari, walizotupasha kwamba: Sisi tu watumwa wake Mungu wa mbingu na nchi; nasi tunaijenga Nyumba hii iliyojengwa kale, sasa yapata miaka mingi, naye aliyeijenga na kuimaliza alikuwa mfalme mkuu wa Waisiraeli. Lakini kwa kuwa baba zetu walimkasirisha Mungu wa mbingu, akawatia mikononi mwa Mkasidi Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, akaibomoa Nyumba hii, nao walio ukoo wake akawateka na kuwahamisha kwenda Babeli. Lakini katika mwaka wa Kwanza wa Kiro, mfalme wa Babeli, mfalme Kiro akatoa amri ya kuijenga tena Nyumba hii ya Mungu. Navyo vyombo vya Nyumba ya Mungu vya dhahabu na vya fedha, Nebukadinesari alivyovitoa Yerusalemu humu Jumbani na kuvipeleka jumbani mle Babeli, mfalme Kiro akavitoa jumbani mle Babeli, akampa mtu aitwaye Sesebasari, aliyemweka kuwa matawala nchi; akamwambia: Hivi vyombo vichukue kwenda navyo, kaviweke Jumbani mle Yerusalemu, nayo Nyumba ya Mungu na ijengwe hapo, ilipokuwa. Ndipo, yule Sesebasari alipokuja, akaiweka misingi ya Nyumba ya Mungu humu Yerusalemu; toka hapo hata leo inajengwa, lakini haijaisha bado. Sasa vikiwa vyema kwake mfalme, na wachunguze nyumbani mwa vilimbiko vya mfalme huko Babeli, kama ni kweli, ya kuwa mfalme Kiro aliagiza kuijenga Nyumba hii ya Mungu humu Yerusalemu. Kisha mfalme na atume kwetu jibu la kutuambia ayatakayo, yafanyike katika jambo hili. Ndipo, mfalme Dario alipotoa amri, wakachunguza nyumbani mwenye vitabu, mlimowekwa navyo vilimbiko vya huko Babeli. Kisha kikaoneka kizingo cha karatasi katika mji wa Ahimeta katika nchi ya Media; ndimo, nalo jumba la mfalme lilimokuwa. Ile karatasi ilikuwa imeandikwa: Ukumbusho. Kwamba: Katika mwaka wa kwanza wa mfalme Kiro huyu mfalme Kiro akatoa amri, Nyumba ya Mungu huko Yerusalemu na ijengwe kuwa mahali, watakapotoa ng'ombe za tambiko, misingi yake itengenezwe kuwa na nguvu; urefu wake uwe mikono sitini, nao upana wake uwe mikono sitini. Waweke masafu matatu ya mawe makubwa ya kuchonga, tena safu moja la mbao mpya; nazo fedha za kulipa wapewe, zitoke nyumbani mwa mfalme. Navyo vyombo vya Nyumba ya Mungu vya dhahabu na vya fedha, Nebukadinesari alivyovitoa Nyumbani mle Yerusalemu na kuvipeleka Babeli, sharti virudishwe, vije Nyumbani mwa Yerusalemu kila kimoja mahali pake na kuwekwa mle Nyumbani mwa Mungu. Sasa wewe Tatinai, mtawala nchi zilizoko ng'ambo ya huko ya jito kubwa, na Setari-Bozinai pamoja na wenzako Waafarsaki walioko ng'ambo ya huko ya jito kubwa, jitengeni, msifike huko! Waacheni, kazi za Nyumba hii ya Mungu ziendelee, mtawala nchi wa Wayuda na wazee wa Wayuda waijenge Nyumba hiyo ya Mungu hapo, ilipokuwa! Mimi natoa amri, ya kwamba msaidiane na hao wazee katika kuijenga Nyumba hiyo ya Mungu, mkifanya bidii, mpate kutoa mali za mfalme zitokazo katika kodi za nchi zilizoko ng'ambo ya huko ya jito kubwa, watu hao wapewe kila mara fedha za kuzilipa hizo hazi, wasizuiliwe. Nayo mengine wanayopaswa nayo, kama madume ya ndama na madume ya kondoo na wana kondoo wa kuwa ng'ombe za tambiko za Mungu wa mbingu, tena ngano na chumvi na mvinyo na mafuta, kama watambikaji walioko Yerusalemu wanavyovitaka, sharti wapewe siku kwa siku, visikoseke, wapate kumtolea mungu wa Mbingu minuko mizuri na kuwaombea wafalme na wana wao, wawe wenye uzima. Tena ninatoa amri kwamba: Kila mtu atakayeligeuza neno hili nyumbani mwake itolewe nguzo, isimikwe, kisha mwenyewe atundikwe humo, nayo nyumba yake igeuzwe kuwa kifusi kwa ajili hiyo. Naye Mungu atakayelikalisha Jina lake mle na awabwage chini wafalme wote na watu wote watakaokunjua mikono yao, waligeuze neno hili, waiharibu Nyumba hiyo ya Mungu iliyomo Yerusalemu. Mimi Dario nimeitoa amri hii, sharti ifanyizwe pasipo kuikosea. Kwa hiyo Tatinai, mtawala nchi zilizoko ng'ambo ya huku ya jito kubwa, na Setari-Bozinai na wenzao wakafanya sawasawa kabisa, kama mfalme Dario alivyowaagiza katika hiyo barua. Nao wazee wa Wayuda wakaendelea kujenga, wakafanikiwa, kama wafumbuaji Hagai na Zakaria, mwana wa Ido, walivyowaambia kwa ufumbuaji wao: wakajenga, hata wakamaliza kwa amri yake Mungu wa Isiraeli na kwa amri za Kiro na za Dario na za Artasasta, wafalme wa Wapersia. Nyumba hii ikamalizika siku ya tatu ya mwezi wa Adari, nao ule mwaka ulikuwa wa sita wa ufalme wa mfalme Dario. Ndipo, wana wa Isiraeli, watambikaji na Walawi nao wale wengine waliotoka kwenye kutekwa walipoieua Nyumba hii ya Mungu kwa furaha. Hapo walipoieua Nyumba hii ya Mungu wakatoa ng'ombe 100 na madume ya kondoo 200 na wana kondoo 400 kuwa ng'ombe za tambiko, tena madume 12 ya mbuzi kwa hesabu ya mashina ya Isiraeli kuwa ng'ombe za tambiko za weuo wa ukoo mzima wa Isiraeli. Kisha wakaweka watambikaji kwa vyama vyao nao Walawi kwa kura zao, walizopigiwa, wamtumikie Mungu mle Yerusalemu, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Mose. Kisha wao waliotoka kwenye kutekwa wakafanya sikukuu ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Kwani watambikaji na Walawi walijitakasa pamoja, wakatakata wote pia, wakawachinjia kondoo wa Pasaka wote waliotoka kwenye kutekwa nao ndugu zao watambikaji nao wao wenyewe. Wana wa Isiraeli waliorudi kwenye kutekwa wakaila pamoja nao waliotaka kumfuata Bwana Mungu wa Isiraeli, waliojitenga, wasijichafue kwa wamizimu wenzao waliokaa kwao katika nchi hii. Wakaifanya hiyo sikukuu ya Mikate isiyochachwa siku saba na kufurahi, kwani Bwana aliwafurahisha kwa kuugeuza moyo wa mfalme wa Asuri, uwaelekee, aishupaze mikono yao katika kazi ya Nyumba ya Mungu aliye Mungu wa Isiraeli. Mambo hayo yalipokwisha, Artasasta, mfalme wa Wapersia, akapata ufalme. Siku zile alikuwako Ezera, mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia, mwana wa Salumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu, mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayoti, mwana wa Zeraya, mwana wa Uzi, mwana wa Buki, mwana wa Abisua, mwana wa Pinehasi, mwana wa Elazari, mwana wa mtambikaji mkuu Haroni. Huyu Ezera akatoka Babeli, akapanda kuja kwao. Alikuwa mwandishi aliye fundi wa Maonyo ya Mose, Bwana Mungu wa Isiraeli aliyoyatoa; kwa kuwa mkono wa Bwana Mungu wake ulikuwa naye, mfalme akampa yote, aliyoyataka. Wakapanda naye wana wa Isiraeli na watambikaji na Walawi na waimbaji na walinda malango na watumishi wa Nyumbani mwa Mungu kwenda Yerusalemu katika mwaka wa saba wa mfalme Artasasta. Akafika Yerusalemu katika mwezi wa tano wa huo mwaka wa saba wa mfalme. Kwani siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza walianza kutoka Babeli na kupanda kwenda zao, tena siku ya kwanza ya mwezi wa tano akafika Yerusalemu, kwa kuwa mkono wa Mungu wake ulikuwa naye, ukamsaidia vema. Kwani Ezera alikuwa ameuelekeza moyo wake kuyatafuta Maonyo ya Bwana, ayafanye, tena awafundishe Waisiraeli maongozi na maamuzi yapasayo. Huu ndio mwandiko wa pili wa ile barua, mfalme Artasasta aliyompa mtambikaji na mwandishi Ezera aliyeyajua vema maneno ya maagizo na ya Maonyo, Bwana aliyowapa Waisiraeli. Artasasta, mfalme wa wafalme, kwa mtambikaji Ezera anayeyajua vema maagizo ya Mungu wa mbingu: Salamu zote na mengine yafuatayo! Mimi nimetoa amri kwamba: katika ufalme wangu kila aliye wa ukoo wa Isiraeli na watambikaji na Walawi, akitaka mwenyewe kwenda Yerusalemu, na aende na wewe! Kwani unatumwa na mfalme na wakuu wake saba wanaokula njama naye, uje kuyachunguza mambo ya Yuda na ya Yerusalemu, kama yanapatana na Maonyo ya Mungu wako yaliyomo mkononi mwako. Tena uzipeleke fedha na dhahabu, mfalme na wakuu wake wanaokula njama naye wanazozitoa kwa kupenda wenyewe, wampe Mungu wa Isiraeli anayekaa Yerusalemu; uzipeleke nazo fedha na dhahabu zote, utakazopewa katika mji wote wa Babeli pamoja na vipaji, watu na watambikaji wenyewe watakavyoitolea Nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu. Kwa hiyo ziangalie vema hizo fedha, kisha zitoe kununua madume ya ndama na madume ya kondoo na wana kondoo navyo vilaji na vinywaji vya tambiko; kisha vyote umtolee Mungu penye meza ya kutambikia katika Nyumba ya Mungu wenu iliyomo Yerusalemu! Kisha fedha na dhahabu zitakazosalia zitumieni, kama wewe na ndugu zako mtakavyoona kuwa vema vya kumtumikia Mungu wenu, apendezwe. Tena vyombo, ulivyopewa vya kutumikia Nyumbani mwa Mungu wako, vyote uvipeleke Yerusalemu kuviweka mbele ya Mungu. Nayo mengine yote, Nyumba ya Mungu wako itakayopaswa nayo, nayo malipo yote yatakayokuangukia wewe, utayapata nyumbani mwenye vilimbiko vya mfalme. Tena mimi mfalme Artasasta ninawatolea amri watunza mali wote walioko ng'ambo ya huko ya jito kubwa kwamba: Yote, mtambikaji Ezera anayeyajua vema Maonyo ya Mungu wa mbingu atakayowaomba ninyi, yafanyike sawasawa, mpaka yapate vipande mia vya fedha, ndio milioni ya shilingi na frasila elfu za ngano na frasila mia za mvinyo na frasila mia za mafuta, tena chumvi pasipo kipimo cho chote. Yote, watakayoyataka kwa amri ya Mungu wa mbingu, sharti yafanyike vizuri, kwa kuwa ni ya Nyumba ya Mungu wa mbingu, ufalme wa mfalme na wanawe wasipatwe na makali yake. Nayo hii ijulike kwenu, ya kuwa hakuna ruhusa kabisa ya kuwatoza kodi, wala ushuru wa forodhani wala wa njiani, walio watambikaji na Walawi na waimbaji na walinda malango na watumishi wa Nyumbani nao wengine wanaoitumikia Nyumba hiyo ya Mungu. Kisha wewe Ezera kwa hivyo, unavyomjua Mungu wako kwa kweli, weka waamuzi na wenye kukata mashauri, wawakatie mashauri yao walio wa ukoo huu wote wanaokaa ng'ambo ya huko ya jito kubwa, wao wayajuao Maonyo ya Mungu wako, nao wasioyajua wawafundishe! Lakini kila mtu asiyeyafanya maagizo ya Mungu wako, nayo maagizo ya mfalme, sharti apatilizwe kwa ukali, kama ni kuuawa au kuhamishwa au kutozwa fedha au kufungwa. Bwana Mungu wa baba zetu na atukuzwe kwa kumpa mfalme moyoni mwake mawazo kama hayo, aipambe Nyumba ya Bwana iliyomo Yerusalemu! Mimi amenipatia upendeleo mbele ya mfalme na mbele ya wakuu wake wanaokula njama naye na mbele ya wakuu wote wa mfalme walio na nguvu; kwa hivyo, mkono wa Bwana Mungu wangu ulivyokuwa na mimi, nimejipa moyo wa kukusanya wakuu wa milango ya Waisiraeli, waje kupanda kwenda kwetu pamoja na mimi. Hawa ndio wakuu wa milango ya baba zao na hesabu ya vizazi vyao waliopanda na mimi kutoka Babeli katika siku za ufalme wa mfalme Artasasta. Kwa wana wa Pinehasi: Gersomu; kwa wana wa Itamari: Danieli; kwa wana wa Dawidi: Hatusi wa wana wa Sekania; kwa wana wa parosi: Zakaria, tena pamoja naye wakaandikwa wa huo udugu waume 150; kwa wana wa Pahati-Moabu: Elihoenai, mwana wa Zeraya, tena pamoja naye waume 200; kwa wana wa Sekania: mwana wa Yahazieli, tena pamoja naye waume 300; kwa wana wa Adini: Ebedi, mwana wa Yonatani, tena pamoja naye waume 50; kwa wana wa Elamu: Yesaya, mwana wa Atalia, tena pamoja naye waume 70; kwa wana wa Sefatia: Zebadia, mwana wa Mikaeli, tena pamoja naye waume 80; kwa wana wa Yoabu: Obadia, mwana wa Yehieli, tena pamoja naye waume 218; kwa wana wa Selomiti: mwana wa Yosifia, tena pamoja naye waume 160; kwa wana wa Bebai: Zakaria, mwana wa Bebai, tena pamoja naye waume 28; kwa wana wa Azgadi: Yohana, mwana wa Katani, tena pamoja naye waume 110; kwa wana wa Adonikamu wako waliochelewa, majina yao ni haya: Elifeleti, Yieli na Semaya, tena pamoja nao waume 60; kwa wana wa Bigwai: Utai na Zabudi, tena pamoja nao waume 70. Nikawakusanya penye mto uendao Ahawa, tukakaa huko kambini siku tatu; nilipowakagua hawa watu na watambikaji, sikuona huko wana wa Lawi. Ndipo, nilipotuma wakuu wa milango, akina Eliezeri, Arieli, Semaya na Elnatani na Yaribu na Elnatani na Natani na Zakaria na Mesulamu na wafunzi Yoyaribu na Elnatani, nikawaagiza kwenda kwa Ido aliyekuwa mkuu wa mlango mahali panapoitwa Kosifia, nikawatia vinywani mwao maneno ya kumwambia Ido na ndugu zake na watumishi wa Nyumbani mwa Mungu walioko kule Kosifia, watuletee watakaoitumikia Nyumba ya Mungu wetu. Kwa kuwa mkono wa Mungu ulikuwa nasi, ukatusaidia vema, wakatuletea mtu mwenye akili wa wana wa Mahali, mwana wa Lawi, mwana wa Isiraeli, naye Serebia na wanawe na ndugu zake, watu 18; tena Hasabia na pamoja naye Yesaya wa wana wa Merari na ndugu zake na wana wao, watu 20; tena watumishi wa Nyumbani mwa Mungu, Dawidi na wakuu waliowapa Walawi, wawatumikie, hawa watumishi wa Nyumbani mwa Mungu walikuwa 220, wao wote walikuwa wameandikwa majina yao. Hapo penye mto wa Ahawa nikatangaza mfungo, tujinyenyekeze mbele ya Mungu wetu na kumwomba, atuongoze sisi na watoto wetu na mali zetu zote kwenye njia inyokayo. Kwani nalipatwa na soni za kumwomba mfalme, atupe kikosi cha askari na wenye kupanda farasi, watusaidie njiani kupigana na adui, kwa maana tulikuwa tumemwambia mfalme kwamba: Mkono wa Mungu wetu huwasimamia wote wamtafutao, uwapatie mema; lakini nguvu zake na makali yake huwatokea wote waliomwacha. Tukafunga mfungo na kumwomba Mungu, atupatie hayo mema, naye akatuitikia. Kisha nikachagua katika wakuu wa watambikaji watu 12, ndio Serebia na Hasabia na pamoja nao ndugu zao kumi, nikawapa na kuzipima zile fedha na dhahabu na vile vyombo, Nyumba ya Mungu wetu ilivyotolewa, walivyovitoa mfalme na wenzake wa njama zake na wakuu wake nao Waisiraeli wote walioonekana huko. Nikawapa mikononi mwao na kuzipima: fedha vipande 650, ndio shilingi kama milioni 7 na 800000, na vyombo vya fedha vipande 100, ndio shilingi kama milioni na 200000, na dhahabu vipande 100, ndio shilingi kama milioni 22; tena vinyweo vya dhahabu 20, kima chao ni dariko 1000, ndio shilingi kama 40000, tena vyombo viwili vizuri vya shaba vilivyometuka kama dhahabu, kima chao kilikuwa sawa na dhahabu. Nikawaambia: Ninyi m watakatifu wa Bwana, navyo hivi vyombo ni vitakatifu, nazo hizi fedha na dhahabu ni vipaji, alivyotolewa Bwana Mungu wa baba zenu. Kwa hiyo mviangalie sana na kuvilinda, mpaka mtakapovitoa na kuwapimia wakuu wa watambikaji na Walawi na wakuu wa milango ya Isiraeli kule Yerusalemu katika vyumba vya kando penye Nyumba ya Bwana. Ndipo, watambikaji na Walawi walipozipokea hizo fedha na dhahabu, walizopimiwa pamoja na vyombo, wavipeleke Yerusalemu katika Nyumba ya Mungu wetu. Kisha tukaondoka hapo penye mto wa Ahawa siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza kwenda Yerusalemu, nao mkono wa Mungu wetu ukatusimamia, ukatuokoa njiani mikononi mwa adui zetu namo mwao wanyang'anyi. Tulipofika Yerusalemu tukapumzika siku tatu. Siku ya nne hizo fedha na dhahabu pamoja na vyombo zikapimwa Nyumbani mwa Mungu wetu, akapewa mtambikaji Meremoti, mwana wa Uria, mkononi mwake; pamoja naye alikuwako Elazari, mwana wa Pinehasi, tena pamoja nao hawa walikuwako Walawi Yozabadi, mwana wa Yesua, na Noadia, mwana wa Binui. Vyote pia vikahesabiwa, vikapimwa, siku hiyo kikaandikwa kipimo chao vyote pamoja. Kisha wao waliorudi kwenye uhamisho, walikopelekwa kwa kutekwa, wakamtolea Mungu wa Isiraeli ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima: ng'ombe dume 12 za Waisiraeli wote, madume ya kondoo 96, wana kondoo 77, tena madume ya kondoo 12 kuwa ng'ombe za tambiko za weuo; hawa wote wakawateketeza kuwa ng'ombe za tambiko za Bwana. Nazo zile amri za mfalme wakawapa watawala nchi wa mfalme na wenye amri waliozishika nchi za ng'ambo ya huku ya jito kubwa; kwa hiyo hawa wakawasaidia hawa watu katika kazi za Nyumba ya Mungu. Hayo yalipomalizika, wakuu wakanitokea kwamba: Walio ukoo wa Isiraeli nao watambikaji na Walawi hawakujitenga kabisa na makabila ya nchi hizi walio na mambo mengi ya kutapisha mtu, wao Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wayebusi, Waamoni, Wamoabu, Wamisri na Waamori. Kwani wamejichukulia wenyewe na wana wao wanawake wa huko; ndivyo, walivyochanganya mazao matakatifu nayo yao ya makabila ya nchi hizi, nao wakuu wa watawalaji ndio walioanza kuinyosha mikono kuyavunja maagano ya Mungu. Nilipolisikia neno hili nikazirarua nguo zangu na kanzu yangu, nikang'oa nywele za kichwani na za udevu, nikaja kukaa chini kwa kupigwa na bumbuazi. Ndipo, walipokusanyika kwangu wote walioingiwa na woga wa ajili ya maneno ya Mungu wa Isiraeli, kwa kuwa wao waliorudi kwenye kutekwa waliyavunja maagano yake; mimi nikawa nimekaa chini kwa kupigwa na bumbuazi, mpaka saa ya tambiko ya jioni ilipofika. Saa ya tambiko ya jioni ilipofika, nikainuka hapo, nilipojinyenyekeza na kuzirarua nguo zangu na kanzu yangu, nikapiga magoti yangu, nikamkunjulia Bwana Mungu wangu mikono yangu, nikasema: Mungu wantu, kwa kutwezwa nina soni za kukuelekezea uso wangu, Mungu wangu, kwani maovu yetu, tuliyoyafanya, ni mengi sana, yanatupita vichwani petu, nazo manza zetu, tulizozikora, ni kubwa, zinafika hata mbinguni. Tangu siku za baba zetu hata siku hii ya leo manza zetu sisi ni kubwa, kwa ajili ya hayo maovu yetu sisi na wafalme wetu na watambikaji wetu tulikuwa tumetiwa mikononi mwa wafalme wa nchi hizi, watuue kwa panga, watuteke, watunyang'anye mali zetu, watutukane usoni petu, kama vinavyofanywa hata leo. Sasa kitambo kidogo huruma imetutokea iliyotoka kwa Bwana Mungu wetu, akisaza kwetu wengine waliopona, tena akitupa kupigilia mambo mahali pake Patakatifu, Mungu wetu akitaka kuyaangaza macho yetu akitupa kupumua kidogo katika utumwa. Kwani sisi tu watumwa, lakini Mungu hakutuacha, ingawa tu watumwa, ila alitupatia upendeleo mbele ya wafalme wa Wapersia, atupe kupumua na kuijenga tena Nyumba ya Mungu wetu na kuyasimamisha tena mabomoko yake na kutupa mahali penye boma, tukae huku Yuda mijini mwa Yerusalemu. Na sasa tusemeje, Mungu wetu, hayo yakifanyika kwetu? Kwani tumeyaacha maagizo yako, uliyotuagiza vinywani mwao watumishi wako wafumbuaji kwamba: Nchi, mtakayoiingia kuichukua, ni nchi yenye uchafu kwa ajili ya machafu ya makabila ya nchi hizo na kwa ajili ya matapisho yao, waliyoyafurikisha huko toka mpaka hata mpaka kwa machukizo yao ya kimizimu. Kwa hiyo msiwaoze wana wao wanawali wenu, wala wana wenu msiwaoze wanawali mwao, wala msiwatafutie kale na kale matengemano na mema yo yote, kusudi ninyi mpate nguvu, myale mema ya nchi hii, mkayaachia wana wenu, yawe fungu lao kale na kale. Kweli haya yote yametupata kwa ajili ya matendo yetu mabaya na kwa ajili ya manza zetu zilizo kubwa; lakini wewe, Mungu wetu, umetupunguzia malipizo yaliyoyapasa maovu yetu, tuliyoyafanya, ukatupatia uponya kama huu. Kwa hiyo inapasaje kuyavunja maagizo yako kwa kuoana na watu wa makabila haya yatapishayo? Hutatutolea makali, mpaka tuangamie kabisa, pasiwepo masao wala uponya? Bwana Mungu wa Isiraeli, wewe u mwongofu; kwani wao waliosalia ni sisi tu tuliopona, kama inavyojulika leo. Tazama, sisi tunasimama mbele yako na kuziungama manza zetu, kwani hakuna awezaye kusimama mbele yako kwa hivyo, alivyo. Ezera alipoomba na kuungama hivyo akilia na kujiangusha chini mbele ya Nyumba ya Mungu, ndipo, walipokusanyika kwake Waisiraeli, ukawa mkutano mkubwa mno, waume na wake na wana, nao hao watu wakalia kilio kikubwa. Kisha akasema Sekania, mwana wa Yehieli, wa wana wa Elamu, akamwambia Ezera: Sisi tumemvunjia Mungu maagano kwa kuoa wanawake wageni wa makabila ya nchi hizi; lakini tena kiko kingojeo, Waisiraeli walicho nacho kwa ajili ya jambo hili. Sasa tufanye agano na Mungu wetu, tuwatoe hao wanawake pamoja na wana waliozaliwa nao kwa shauri lako, bwana wangu, na kwa shauri lao wanaoyaogopa maagizo ya Mungu wetu, kisha na yafanywe, kama Maonyo yanavyoyataka. Inuka! Kwani jambo hili linakupasa wewe, sisi nasi tutakuwa upande wako; jipe moyo, uyafanye! Ndipo, Ezera alipoinuka, akawaapisha wakuu wa watambikaji nao wa Walawi na watu wote wa Isiraeli kufanya hivyo, nao wakaapa. Kisha Ezera akaondoka hapo mbele ya Nyumba ya Mungu, akaingia chumbani mwa Yohana, mwana wa Eliasibu; alipofika humo, hakula chakula, wala hakunywa maji, kwani alikuwa amesikitika kwa hilo kosa lao waliorudi kwenye kutekwa, kwani waliyavunja maagano. Kisha wakapiga mbiu katika nchi ya Yuda namo Yerusalemu kwamba: Wote waliorudi kwenye kutekwa wakusanyike Yerusalemu! Kila asiyekuja katika muda wa siku tatu kwa shauri hili lao wakuu na wazee, basi, mali zake zote zitatiwa mwiko wa kuwa mali ya mtu, naye mwenyewe atatengwa katika mkutano wao waliorudi kwenye kutekwa. Ndipo, walipokusanyika Yerusalemu waume wote wa Yuda na wa Benyamini katika muda wa siku tatu, ikawa siku ya ishirini ya mwezi wa tisa. Watu wote wakakaa uwanjani penye Nyumba ya Mungu, wakatetemeka kwa ajili ya jambo hilo, tena kwa kunyewa na mvua nyingi. Hapo mtambikaji Ezera akaondokea, akawaambia: Mmevunja maagano mlipooa wanawake wageni, mkaziongeza manza za Waisiraeli. Sasa mwungamieni Bwana Mungu wa baba zenu! Kisha mfanye yampendezayo, mkijitenga na makabila ya nchi hii, mkijitenga nao wanawake wageni. Mkutano wote pia wakamwitikia na kupaza sauti sana kwamba: kweli inatupasa kuyafanya, uliyoyasema; Lakini watu ni wengi, tena sasa ni masika, watu wasiweze kusimama nje, nayo kazi hii si ya siku moja au mbili, kwani tumezidisha kufanya maovu katika jambo hili. Wakuu wetu na waondokee kuupigia mkutano wote shauri hili, kisha wote waliooa wanawake wageni mijini mwetu na waje siku zitakazowekwa; tena pamoja nao na waje hata wazee na waamuzi wa kila mji, mpaka watakapoyatuliza makali hayo ya Mungu wetu yawakayo moto kwa ajili ya jambo hili, yakatuacha. Waliovibishia hivi walikuwa Yonatani tu, mwana wa Asaheli, na Yahazia, mwana wa Tikwa, naye Mesulamu na Mlawi Sabutai wakawasaidia. Lakini wao wengine waliorudi kwenye kutekwa wakafanya hivyo; wakachaguliwa mtambikaji Ezera na wakuu wa milango ya baba zao, nao wote wakaandikwa majina. Kisha siku ya kwanza ya mwezi wa kumi wakaja kukaa pamoja, walichunguze jambo hili, wakayamaliza mashauri haya ya watu wote waliooa wanawake wageni mpaka siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza. Kwao wana wa watambikaji waliooneka, ya kuwa walioa wanawake wageni, ndio hawa: kwa wana wa Yesua, mwana wa Yosadaki, na kwa ndugu zake: Masea na Eliezeri na Yaribu na Gedalia. Hawa wakaapa na kupeana mikono, ya kuwa watawaondoa wake zao, tena kwa manza zao, walizozikora, wakatoa dume la kondoo kuwa ng'ombe yao ya tambiko ya upozi. Nako kwa wana wa Imeri: Hanani na zebadia. Nako kwa wana wa Harimu: Masea na Elia na Semaya na Yehieli na Uzia. Nako kwa wana wa Pashuri: Eliyoenai, Masea, Isimaeli, Netaneli, Yozabadi na Elasa. Tena kwa Walawi: Yozabadi na Simei na Kelaya aitwaye Kelita, Petaya, Yuda na Eliezeri. Nako kwa waimbaji: Eliasibu; nako kwa walinda malango: Salumu na Telemu na Uri. Nako kwa Waisiraeli wengine: kwa wana wa Parosi: Ramia na Izia na Malkia na Miyamini na Elazari na Malkia na Benaya. Nako kwa wana wa Elamu: Matania, Zakaria na Yehieli na Abudi na Yeremoti na Elia. Nako kwa wana wa Zatu: Eliyoenai, Eliasibu, Matania na Yeremoti na Zabadi na Aziza. Nako kwa wana wa Bebai: Yohana, Hanania, Zabai, Atilai. Nako kwa wana wa Bani: Mesulamu, Maluki na Adaya, Yasubu na Sali, Yeremoti. Nako kwa wana wa Pahati-Moabu: Adina na Kelali, Benaya, Masea, Matania, Besaleli na Binui na Manase. Nako kwa wana wa Harimu: Eliezeri, Isia, Malkia, Semaya, Simeoni, Benyamini, Maluki, Semaria. Kwa wana wa Hasumu: Matinai, Matata, Zabadi, Elifeleti, Yeremai, Manase, Simei. Kwa wana wa Bani: Madai, Amuramu na Ueli, Benaya, Bedia, Keluhi, Wania, Meremoti, Eliasibu, Matania, Matinai na Yasai, na Bani na Binui, Simei, na Selemia na Natani na Adaya, Makinadebai, Sasai, Sarai, Azareli na Selemia, Semaria, Salumu, Amaria, Yosefu. Kwa wana wa Nebo: Yieli, Matitia, Zabadi, Zebina, Yadai na Yoeli na Benaya. Hawa wote walikuwa wamechukua wanawake wageni, namo mwao hao walikuwamo wanawake waliozaa watoto. Haya ni mambo ya Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa katika mwezi wa Kisilewu wa mwaka wa ishirini, nilipokuwa Susani mlimo na jumba la mfalme. Ndipo, alipokuja Hanani, mmoja wao ndugu zangu, pamoja na watu waliotoka Yuda. Nikawauliza habari za Wayuda waliopona, ndio wale waliosalia, wenzao walipohamishwa, na habari za Yerusalemu. Wakaniambia: Yale masao ya watu waliosalia kule jimboni, wenzao walipohamishwa, wamo katika mabaya mengi yawatiayo soni: boma la Yerusalemu lingaliko limebomolewa, nayo malango yake yako vivyo hivyo, yalivyoteketezwa kwa moto. Nilipoyasikia maneno haya, nikakaa siku zile na kulia machozi kwa kusikitika, nikawa mikifunga mfungo na kumwomba Mungu wa mbinguni, nikasema: E. Bwana Mungu wa mbinguni, u Mungu mkubwa, unaogopesha, lakini wao wakupendao na kuyashika maagizo yako unawatimilizia Agano lako na upole wako. Sasa sikio lako na liwe limetegwa, nayo macho yako na yawe wazi, uyasikilize malalamiko ya mtumwa wako, nikulalamikiayo mimi leo mchana na usiku kwa ajili ya wana wa Isiraeli walio watumwa wako, nikikutolea makosa yao wana wa Isiraeli, tuliyokukosea, mimi nami nao wa mlango wa baba yangu tumekosa. Tumekufanyizia maovu mengi, hatukuyashika maagizo, wala maongozi, wala maamuzi yako, uliyomwagiza mtumishi wako Mose. Likumbuke lile neno, ulilomwagiza mtumishi wako Mose la kwamba: Mtakapoyavunja maagano, mimi nitawatapanya kwenye makabila yote; lakini mtakaporudi kwangu na kuyashika maagizo yangu, myafanye, nitawakusanya, ijapo mwe mmekimbizwa mpaka kwenye mapeo ya mbingu; huko nako nitawatoa na kuwapeleka mahali hapo, nilipopachagua, pawe pa kulikalishia Jina langu. Nao ndio watumwa wako na ukoo wako, uliowakomboa kwa nguvu zako kuu na kwa mkono wako unaoshupaa. E Bwana, sasa sikio lako na liwe limetegewa maombo ya mtumwa wako na malalamiko ya watumwa wako wanaopendezwa na kulicha Jina lako! Umfanikishe leo mtumwa wako na kumhurumia machoni pa mtu huyu! Kwani nilikuwa mtunza vinywaji kwake mfalme. Ikawa katika mwezi wa Nisani wa mwaka wa ishirini wa mfalme Artasasta; hapo, mvinyo ilipowekwa mbele yake, nikaichukua hiyo mvinyo, nikampa mfalme; lakini mpaka hapo sijawa nikinuna mbele yake. Mfalme akaniuliza: Mbona uso wako unanuna, ukiwa huugui? Hili si jingine, ila ni sikitiko la moyo. Ndipo, nilipoingiwa na woga mwingi sana, nikamjibu mfalme: Mfalme na awe mwenye uzima kale na kale! Je? Uso wangu usinune, mji ulio na makaburi ya baba zangu ukiwa umebomoka, nayo malango yake yakiwa yameteketezwa kwa moto? Mfalme akaniuliza: Sasa wewe unatakaje? Ndipo, nilipomwomba Mungu wa mbinguni, nikamwambia mfalme: Vikiwa vema machoni pako, mfalme, mtumwa wako naye akiwa mwema machoni pako, nitume, niende katika nchi ya Yuda mle mjini mlimo na makaburi ya baba zangu, miujenge! Mfalme akaniuliza, naye mkewe alikuwa amekaa kando yake, kwamba: Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Utarudi lini? Basi, mfalme akaviona kuwa vema, akanituma, nami nikaagana naye siku za kurudi. Kisha nikamwambia mfalme: Vikiwa vema kwake mfalme, na wanipe barua za kuwapelekea wenye amri walioko ng'ambo ya huko ya jito kubwa, waniache, nipite, mpaka nitakapofika Yuda. Tena barua kwa Asafu, mtunza miitu ya mfalme, anipe miti ya kutengeneza nguzo za malango ya boma lililoko penye hiyo Nyumba, nayo ya ukuta wa mji na ya nyumba yangu, nitakamoingia. Mfalme akanipa, kwa kuwa mkono wa Mungu wangu ulio mwema ulikuwa na mimi. Nilipofika kwao wenye amri ng'ambo ya huku ya jito kubwa, nikawapa zile barua za mfalme. Tena mfalme alikuwa amenipa hata wakuu wenye vikosi vya askari nao wapanda farasi. Sanibalati wa Horoni na mtumishi Tobia wa Waamoni walipoyasikia haya, wakakasirika sanasana, ya kuwa amekuja mtu aliyetaka kuwatafutia wana wa Isiraeli mema. Nilipofika Yerusalemu nikakaa huko siku tatu. Kisha nikainuka usiku mimi na watu wachache, niliokuwa nao; lakini hakuwako mtu, niliyemwambia Mungu wangu aliyonitia moyoni, niyafanyize Yerusalemu, hata nyama sikuwa naye, isipokuwa yule, niliyempanda. Nikatoka usiku huo katika lango la Bondeni, nikashika njia ya kwenda penye kisima cha Joka na penye lango la Jaani, nikawa nikizichungulia kuta za Yerusalemu zilizokuwa zimebomolewa, nayo malango yaliyokuwa yameliwa na moto. Nikaendelea, nikafika penye lango la Jicho la Maji, hata penye ziwa la mfalme, lakini nyama, niliyempanda, hakuona mahali pa kupitia. Ndipo, nilipokwea katika bonde la kijito usiku uleule, nikawa nikiuchungulia ukuta; kisha nikarudi, nikafika tena kwenye lango la Bondeni, nikarudi nyumbani. Lakini wakuu hawakujua, wala nilikokwenda, wala niliyoyafanya; nami mpaka hapo sikuwaambia Wayuda neno lo lote, wala watambikaji, wala wakuu wa mji, wala watawalaji, wala wao wengine, niliowatakia kazi. Nikawaambia: Mnayaona haya mabaya yaliyotupata, ya kuwa Yerusalemu ni mabomoko, nayo malango yake yameteketezwa kwa moto. Haya! Njoni, na tulijenge boma la Yerusalemu, tusiendelee kutukanwa! Nikawasimulia, mkono wa Mungu ulio mwema ulivyonisaidia, nayo yale maneno, mfalme aliyoniambia. Ndipo, walipoitikia kwamba: Na tuinuke, tujenge! Nayo mikono yao wakaishupaza kufanya kazi njema. Lakini Sanibalati wa Horoni na mtumishi Tobia wa Waamoni na Mwarabu Gesemu walipoyasikia, wakatucheka na kutubeza wakisema: Hii kazi yenu, mnayoifanya, ni ya nini? Mwataka kumkataa mfalme na kuacha kumtii? Nikawajibu neno nikiwaambia: Mungu wa mbinguni atatupa kuimaliza kazi hii; sisi tulio watumwa wake tutainuka, tujenge. Lakini ninyi hamna fungu humu Yerusalemu wala cho chote kilicho chenu wala ukumbusho tu. Ndipo, alipoondokea mtambikaji mkuu Eliasibu pamoja na ndugu zake waliokuwa watambikaji, wakalijenga lango la Kondoo. Kisha wakalieua, wakaitia milango yake, kisha wakajenga kufikia penye mnara wa Hamea, wakaueua, wakaendelea kujenga kufikia penye mnara wa Hananeli. Mkononi kwake kumoja wakajenga watu wa Yeriko, mkononi kwake kungine akajenga Zakuri, mwana wa Imuri. Lango la Samaki wakalijenga wana wa Senaa; walipokwisha kuiunga mihimili yake, wakaitia milango yake na makomeo yake na miti yake ya kukingia. Mkononi kwao kumoja akafanya kazi Meremoti, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, mkononi kwao kungine akawa Mesulamu, mwana wa Berekia, mwana wa Mesezabeli, akifanya kazi, kando yao akawa Sadoki, mwana wa Baana, akifanya kazi. Kando yao hao Watekoa wakafanya kazi, lakini watukufu wa kwao hawakuziinamisha shingo zao kumfanyizia bwana wao kazi. Lango la Kale wakalitengeneza Yoyada, mwana wa Pasea, na Mesulamu mwana wa Besodia; walipokwisha kuiunga mihimili yake wakaitia milango yake na makomeo yake na miti yake ya kukingia. Kando yao wakafanya kazi: Melatia wa Gibeoni na Yadoni wa Meronoti na watu wa Gibeoni na wa Misipa, wakapatengeneza hapo penye kiti cha kifalme cha mwenye amri wa nchi zilizoko ng'ambo ya huku ya jito kubwa. Kando yao wakafanya kazi Uzieli, mwana wa Harihaya, pamoja na wafua dhahabu; kando yake akafanya kazi Hanania, mwana wa chama cha watengeneza manukato; nao wakaujenga Yerusalemu mpaka penye Ukuta Mpana. Kando yake akafanya kazi Refaya, mwana wa Huri, aliyekuwa mkuu wa nusu ya mtaa wa Yerusalemu. Kando yake akafanya kazi Yedaya, mwana wa Harumafu, hapo palipoielekea nyumba yake; kando yake akafanya kazi Hatusi, mwana wa Hasabunia. Kipande kingine wakakifanyizia kazi Malkia, mwana wa Harimu, na Hasabu, mwana wa Pahati-Moabu, wakautengeneza nao mnara wa Tanuru. Kando yake akafanya kazi Salumu, mwana wa Halohesi, aliyekuwa mkuu wa nusu ya pili ya mtaa wa Yerusalemu, yeye na wanawe wa kike. Lango la Bondeni wakalitengeneza Hanuni na wenyeji wa Zanoa; walipokwisha kulijenga, wakaitia milango yake na makomeo yake na miti yake ya kukingia, kisha wakatengeneza mikono elfu ya boma mpaka lango la Jaani. Lango la Jaani akalitengeneza Malkia, mwana wa Rekabu, aliyekuwa mkuu wa mtaa wa Beti-Keremu, alipokwisha kulijenga, akalitia milango yake na makomeo yake na miti yake ya kukingia. Lango la Jicho la Maji akalitengeneza Saluni, mwana wa Koli-Hoze, aliyekuwa mkuu wa mtaa wa Misipa; alipokwisha kulijenga na kulifunika juu, akaitia milango yake na makomeo yake na miti yake ya kukingia; kisha akaujenga ukuta penye ziwa la Sela karibu ya bustani ya mfalme mpaka penye ngazi inayoshuka toka mjini kwa Dawidi. Nyuma yake akafanya kazi Nehemia, mwana wa Azibuku, aliyekuwa mkuu wa nusu ya mtaa wa Beti-Suri mpaka hapo panapoyaelekea makaburi ya Dawidi penye lile ziwa lililotengenezwa hapo, tena mpaka nyumba ya mafundi wa vita. Nyuma yake wakafanya kazi Walawi: Rehumu, mwana wa Bani; kando yake akafanya kazi Hasabia, mkuu wa nusu ya mtaa wa Keila, ni kazi iliyoupasa mtaa wake. Nyuma yake wakafanya kazi ndugu zao: Bawai, mwana wa Henadadi, aliyekuwa mkuu wa nusu ya pili ya mtaa wa Keila. Kando yake akafanya kazi Ezeri, mwana wa Yesua, aliyekuwa mkuu wa Misipa, akatengeneza kipande kingine kielekeacho pa kupandia penye nyumba ya mata huko pembeni. Nyuma yake akafanya kazi na kujihimiza Baruku, mwana wa Zabai, akatengeneza kipande kingine kutoka hapo pembeni kufikia mlango wa nyumba ya mtambikaji mkuu Eliasibu. Nyuma yake akafanya kazi Meremoti, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, akatengeneza kipande kingine kutoka mlango wa nyumba ya Eliasibu kufikia mwisho wa nyumba ya Eliasibu. Nyuma yake wakafanya kazi watambikaji waliokaa katika nchi ya tambarare. Nyuma yao wakafanya kazi Benyamini na Hasubu, wakapatengeneza panapoielekea nyumba yao; nyuma yao wakafanya kazi Azaria, mwana wa Masea, mwana wa Anania, kando ya nyumba yake. Nyuma yake akafanya kazi Binui, mwana wa Henadadi, akatengeneza kipande kingine kutoka nyumba ya Azaria mpaka pembeni panapogeuka. Palali, mwana wa Uzai, akapajenga panapoelekea hapo pembeni na mnara wa juu unaotokea penye nyumba ya mfalme karibu ya uani pa kifungoni. Nyuma yake akajenga Pedaya, mwana wa Parosi. Watumishi wa Nyumbani mwa Mungu walikuwa wanakaa Ofeli kufikia hapo panapoelekea lango la Maji lililoko upande wa maawioni kwa jua, ni hapo panapotokea mnara. Nyuma yao wakafanya kazi Watekoa, wakatengeneza kipande kingine kutoka panapoelekea ule mnara mkubwa unapotokea kufikia ukuta wa Ofeli. Juu ya lango la Farasi wakafanya kazi watambikaji, kila mmoja akapatengeneza panapoielekea nyumba yake. Nyuma yao akafanya kazi Sadoki, mwana wa Imeri, akapatengeneza panapoielekea nyumba yake; nyuma yake akafanya kazi semaya, mwana wa Sekania, mlinzi wa lango lielekealo upande wa maawioni kwa jua. Nyuma yake wakafanya kazi Hanania, mwana wa Selemia, na Hanuni, mwana wa sita wa Salafu, wakatengeneza kipande kingine. Nyuma yake akafanya kazi Mesulamu, mwana wa Berekia, akapatengeneza panapokielekea chumba chake. Nyuma yake akafanya kazi Malkia, mwana wa chama cha wafua dhahabu, akatengeneza kipande kuifikia nyumba ya watumishi wa Nyumbani mwa Mungu na ya wachuuzi, ni hapo panapoelekea lango la Ukaguzi hata pa kupandia pembeni. Tena hapo katikati ya kupandia pembeni na lango la Kondoo wakapatengeneza wafua dhahabu na wachuuzi. Ikawa, Sanibalati aliposikia, ya kuwa sisi tunalijenga boma, ndipo, makali yake yalipowaka moto, akakasirika sana, akawafyoza Wayuda. Akasema mbele ya ndugu zake na mbele ya vikosi vya Samaria kwamba: Hawa Wayuda wasio na nguvu wanafanya nini? Je Wanajijengea wenyewe? Watatoa hapo ng'ombe za tambiko? Je? Siku itafika, watakapozimaliza kazi hizo? Nayo mawe watawezaje kuyafufua katika machungu ya mavumbini? Nayo yamekwisha kuteketea kale! Baadaye Mwamoni Tobia aliyesimama kando yake akasema: Yo yote, watakayoyajenga, kama mbwa wa mwitu tu atayapandia, atayatawanya mawe ya boma lao. Mungu wetu, sikia, jinsi sisi tulivyowageukia kuwa wa kubezwa tu! Kawarudishie matusi yao vichwani pao ukiwatoa, wanyang'anywe mali zao katika nchi, watakakotekwa! Wala usizifunike manza zao, walizozikora, wala makosa yao yasifutwe usoni pako! Kwani mbele yao hawa wanaojenga wamesema maneno ya kukasirisha. Basi, tukalijenga boma; kuta zote za boma zilipopandishwa na kufika katikati ya urefu wa juu, watu wakajikaza kujenga. Ikawa, Sanibalati na Tobia na Waarabu na Waamoni na Waasdodi waliposikia, ya kuwa jengo la kuta za boma la Yerusalemu linaendelea, ya kuwa wameanza kupaziba palipokuwa pamebomoka, makali yao yakawaka moto. Wakaapiana wote pamoja kuja Yerusalemu kupigana nao na kuwafanyia matata. Tukamlalamikia Mungu, tukaweka walinzi po pote, wawalindie mchana na usiku. Wayuda wakasema: Nguvu za wachukuzi zimekwisha, hujikwaa tu, nayo mavumbi ni mengi, kwa hiyo hatuwezi kuendelea kulijenga boma. Nao wapingani wetu wakasema: Wasijue, wala wasituone, mpaka tutokee katikati yao na kuwaua, wazikomeshe kazi zao! Lakini Wayuda waliokaa kandokando yao walipotuambia hata mara kumi wakitoka po pote vijijini mwao: Sharti mrudi kwetu, ndipo, nilipoweka watu nyuma ya boma mahali pakavu palipokuwa chini kidogo, hapo nikawaweka milango kwa milango wenye panga na mikuki na pindi zao. Nikawatazama, kisha nikaondoka, nikawaambia wakuu wa miji na watawalaji na watu wote wengine pia: Msiwaogope! Ila mkumbukeni Bwana aliye mkuu mwenye kuogopesha! Wapiganieni ndugu zenu na wana wenu wa kiume na wa kike na wake zenu na nyumba zenu! Adui zetu walipokwisha kusikia, ya kuwa tumeyajua mambo yao, ya kuwa Mungu amelivunja shauri lao, basi, sisi tukarudi sote kwenye boma kila mtu kwa kazi yake. Tangu siku hiyo waliofanya kazi walikuwa nusu tu ya vijana wangu, nusu yao wengine walishika mikuki na ngao na pindi na shati zao za vyuma, nao wakuu wakawasimamia watu wote wa mlango wa Yuda, waliolijenga boma. Lakini wachukuzi waliopagaa mizigo kwa mkono mmoja wakafanya kazi, kwa mkono mwingine wakashika mata. Nao waliojenga kila mtu akawa amejifunga upanga wake kiunoni pake, naye mpiga baragumu akawa amesimama kando yangu. Nikawaambia wakuu wa miji na watawalaji na watu wengine wote pia: Hapa, tunapofanyia kazi zetu za kujenga, ni parefu mno, nasi tuko tumetawanyika ukutani, tunasimama mbali kidogo, kila mtu na mwenziwe; kwa hiyo hapo, mtakaposikia, baragumu likilia mahali, paendeeni, mkusanyike kwetu sisi! Naye Mungu wetu atatupigia vita hivi. Ndivyo, tulivyozifanya kazi zetu, nusu yao wakishika mikuki tangu hapo, jua lilipokucha, hata nyota zilipotokea. Hapo ndipo, nilipowaambia watu: Kila mtu na kijana wake sharti walale humu Yerusalemu, na usiku wawe walinzi, tena mchana wafanye kazi! Hapo wala mimi wala ndugu zangu wala vijana wangu wala walinzi walionifuata, sisi sote hatukuzivua nguo zetu; hata tulipokwenda mtoni, kila mtu alishika mata yake. Kukawa na kilio kikubwa cha watu na cha wake zao kwa ajili ya ndugu zao Wayuda. Wakawako waliosema: Sisi wana wetu wa kiume na wa kike ni wengi, sharti tupate ngano, tule, tusife. Walikuwako nao wengine waliosema: Mashamba yetu na mizabibu yetu na nyumba zetu hatuna budi kuzitoa kuwa rehani, tupate ngano katika njaa hii. Tena walikuwako wengine waliosema: Tumeyatoa mashamba yetu na mizabibu yetu tulipokopa fedha za kulipa kodi ya mfalme. Sasa miili yetu si sawa na miili yao ndugu zetu? Nao wana wetu si sawa na wana wao? Tena inakuwaje, tusipokuwa na budi sisi kuwashurutisha wana wetu wa kiume na wa kike kuwa watumwa? Kweli wako wana wetu wa kike waliouzwa utumwani, namo mikononi mwetu hamna cho chote, kwani mashamba yetu na mizabibu yetu ni ya wengine. Makali yangu yakawaka moto, nilipokisikia hicho kilio chao na maneno hayo. Nikapiga shauri moyoni, nikawagombeza wakuu wa miji na watawalaji nikiwaambia: Ninyi mnawachuuzia vibaya, kila mtu na ndugu yake. Nikawakusanya kuwa mkutano mkubwa na kuteteana nao, nikawaambia: Sisi tuliwakomboa ndugu zetu wa Kiyuda wlaiouzwa kwa wamizimu, kama tulivyoweza; nanyi mtawauza ndugu zenu, waje kujiuza kwetu sisi! Wakanyamaza kimya, hawakuona la kujibu. Nikasema: Halifai jambo hili, mnalolifanya ninyi; je? Haiwapasi kufanya mwenendo wa kumwogopa Mungu wetu, adui zetu wa kimizimu wasitutukane? Mimi nami na ndugu zangu na vijana wangu tunawakopesha fedha na ngano; lakini sasa deni hizi na tuwaachilie! Warudishieni siku hii ya leo mashamba yao na mizabibu yao na michekele yao na nyumba zao nazo faida, mlizowatoza za fedha na za ngano na za mvinyo mbichi na za mafuta! Wakaitikia kwamba: Tutavirudisha, tusitake kwao cho chote. Tufanye hivyo, kama unavyosema wewe! Nikawaita watambikaji, nikawaapisha, ya kwamba wafanye, kama walivyosema. Kisha nikaikung'uta mikunjo ya nguo zangu nikisema: Hivi ndivyo, Mungu atakavyomkung'uta kila mtu asiyelitimiza neno hili, atoke nyumbani mwake, nayo mapato yake yamtoke; kweli ndivyo, atakavyokung'utwa, awe pasipo kitu kabisa. Mkutano wote ukaitikia: Amin, kisha wakamsifu Bwana, watu wakafanya, kama walivyosema. Tangu siku ile, mfalme aliponiweka kuwa mtawala nchi kwao katika nchi ya Yuda, ni tangu mwaka wa ishirini hata mwaka wa thelathini na mbili wa mfalme Artasasta, hii miaka kumi na miwili, wala mimi wala ndugu zangu hatukula chakula cha mtawala nchi. Lakini wenye amri walionitangulia waliwalemeza watu wakichukua kwao kila siku chakula na mvinyo za fedha arobaini na zaidi; vijana wao nao waliwakorofisha watu. Lakini mimi sikufanya kama hayo kwa kumwogopa Mungu. Hata katika hili jengo la boma nilifanya kazi, lakini hatukununua shamba la watu, nao vijana wangu walikuwa wamekusanywa hapo penye jengo hilo. Tena mezani pangu wakala Wayuda na wakuu, watu 150, nao waliokuja kwetu wakitoka kwa wamizimu wanaokaa na kutuzunguka. Navyo vyakula vilivyoandaliwa vya kila siku moja, vilikuwa ng'ombe mmoja na kondoo sita waliochaguliwa vema na kuku pia, tena kila siku kumi mvinyo nyingi za kila namna. Kwa hayo yote sikutaka chakula cha mtawala nchi, kwani utumishi uliwalemea watu hawa. Mungu wangu, unikumbukie hayo, unirudishie mema kwa ajili ya hayo yote, niliyowafanyizia watu hawa! Kisha Sanibalati na Tobia na Mwarabu Gesemu nao adui zetu wengine wakasikia, ya kuwa nimelijenga boma, usisalie ufa humo; lakini siku zile sijatia bado milango malangoni. Ndipo, Sanibalati na Gesemu walipotuma kwangu kwamba: Njoo, tukutane pamoja penye vijiji vilivyomo bondeni kwa Ono! Kwani waliwaza kunifanyizia mabaya. Nikatuma wajumbe kwao kwamba: Mimi nina kazi kubwa ya kuifanya, kwa hiyo siwezi kushuka. Mbona niiache kazi hii, ikome, nikishuka kuja kwenu? Wakatuma kwangu kama mara nne kuniambia maneno yayo hayo, nami nikawajibu yayo hayo. Kisha Sanibalati akatuma kijana wake kwangu mara ya tano kuniambia yayo hayo, hata barua iliyo wazi ilikuwa mkononi mwake. Humo yalikuwa yameandikwa haya: Katika wamizimu yanasimuliwa, naye Gasemu anayasema, ya kuwa wewe na wayuda mnawaza kumwinukia mfalme, kwa sababu hii unalijenga boma, wewe upate kuwa mfalme wao, na mengine kama hayo. Umeweka hata wafumbuaji, wakutangaze mle Yerusalemu kwamba: Huyu ni mfalme katika nchi ya Yuda! Maneno kama hayo mfalme naye atasimuliwa, kwa hiyo njoo sasa, tupige shauri pamoja! Kisha nikatuma kwake kwamba: Mambo kama hayo, unayoyasema wewe, hayakufanyika, ila wewe unayatunga mwenyewe moyoni mwako. Kwani wao wote walitaka kutuogopesha tu kwa kwamba: Hivyo mikono yao italegea, isifanye kazi, jengo hilo lisimalizike. Sasa wewe Mungu, ishupaze mikono yetu! Mimi nikaenda kuingia nyumbani mwa Semaya, mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, naye alikuwa amefungiwa; akaniambia: Na tukutane Nyumbani mwa Mungu, katikati ya Jumba hilo, tuifunge milango ya Jumba hilo, kwani wako wanaokuja kukuua, nao watakuja usiku huu, wakuue. Nikamjibu: Mtu kama mimi anawezaje kutoroka? Tena mtu kama mimi akiingia humo Jumbani atawezaje kupona? Sitakuja. Nalikuwa nimetambua, nikaona, ya kuwa siye Mungu aliyemtuma, aniambie huo ufumbuaji, ila Tobia na Sanibalati walikuwa wamempenyezea mali. Naye alipenyezewa mali, kusudi niingiwe na woga, niyafanye hayo ya kumkosea Mungu, wapate kulitokeza jina langu kuwa baya, wanitukane. Mungu wangu, yakumbuke hayo matendo ya Tobia na ya Sanibalati! Mkumbuke naye mfumbuaji mke Noadia na wale wafumbuaji wengine waliotaka kuniogopesha! Boma likamalizika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli kwa siku hamsini na mbili. Adui zetu wote walipoyasikia haya, wakaogopa wao wamizimu wote waliokaa na kutuzunguka, wakazimia kabisa machoni pao kwa kujua, ya kuwa jengo hilo limefanywa kwa nguvu zitokazo kwake Mungu. Tena katika siku hizo, walikuwako wakuu wa miji ya Wayuda waliompelekea Tobia barua nyingi, nazo za Tobia zikafika kwao. Kwani katika nchi ya Yuda walikuwako wengi waliomwapia kumsaidia, kwani alikuwa mkwewe Sekania, mwana wa Ara; naye mwanawe Yohana alimwoa binti Mesulamu, mwana wa Berekia. Mimi nami wakanisimulia mambo yake mema, nayo niliyoyasema wakamtolea. Hata Tobia mwenyewe akatuma kwangu barua za kuniogopesha. Ikawa, boma lilipokwisha kujengwa, nikatia milango, wakawekwa walinda malango na waimbaji na Walawi, nikamwagiza ndugu yangu Hanani na Hanania, mkuu wa boma, kushika amri humu Yerusalemu, kwani huyu alikuwa mtu mwelekevu mwenye kumcha Mungu kuliko wengine wengi. Nikawaambia: Malango ya Yerusalemu yasifunguliwe, mpaka jua liwake na nguvu; tena walinzi wakingali wanasimama, malango yafungwe na kutiwa makomeo. Tena mweke wenyeji wa Yerusalemu kuwa walinzi kila mtu na zamu yake ya kulinda hapo panapoielekea nyumba yake. Lakini mji ulikuwa mpana pande zote na mkubwa, lakini watu waliomo walikuwa wachache, hata nyumba mpya hazikujengwa. Mungu akanitia moyoni, niwakusanye wakuu wa miji na watawalaji nao watu, waandikwe milango yao. Nikaona chuo kilichoandikwa udugu wao walionza kurudi na kupanda huku, nikaona yameandikwa haya: Hawa ndio watu waliokaa majimboni waliporudi kutoka mafungoni kwenye kutekwa; ndio wao, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, aliowateka na kuwahamisha, nao wakapata kurudi Yerusalemu na Yuda, kila mtu mjini kwake. Walikuja pamoja nao Zerubabeli, Yesua, Nahemia, Azaria, Ramia, Nehamani, Mordekai, Bilsani, Misipereti, Bigwai, Nehumu na Baana. Hesabu ya waume wa Waisiraeli ni hii: Wana wa Parosi 2172; wana wa Sefatia 372; wana wa Ara 652; wana wa Pahati-Moabu, ndio wana wa Yesua na wa Yoabu, 2818; wana wa Elamu 1254; wana wa Zatu 845; wana za Zakai 760; wana wa Binui 648; wana wa Bebai 628; wana wa Azgadi 2322; wana wa Adonikamu 667; wana wa Bigwai 2067; wana wa Adini 655; wana wa Ateri walio wa Hizikia 98; wana wa Hasumu 328; wana wa Besai 324; wana wa Harifu 112; wana wa Gibeoni 95; waume wa Beti-Lehemu na wa Netofa 188; waume wa Anatoti 128; waume wa Beti-Azimaweti 42; waume wa Kiriati-Yearimu, wa Kefira na wa Beroti 743; waume wa Rama na wa Geba 621; waume wa Mikimasi 122; waume wa Beteli na wa Ai 123; waume wa Nebo wa pili 52; wana wa Elamu wa pili 1254; wana wa Harimu 320; wana wa Yeriko 345; wana wa Lodi, wa Hadidi na wa Ono 721; wana wa Senaa 3930. Watambikaji walikuwa hawa: wana wa Yedaya wa mlango wa Yesua 973; wana wa Imeri 1052; wana wa Pashuri 1247; wana wa Harimu 1017. Walawi walikuwa hawa: wana wa Yesua wa mlango wa Kadimieli na wana wa Hodawia 74. Waimbaji walikuwa wana wa Asafu 148. Walinda malango walikuwa wana wa Salumu, wana wa Ateri, wana wa Talmoni, wana wa Akubu, wana wa Hatita, wana wa Sobai, watu 138. Watumishi wa Nyumbani mwa Mungu walikuwa hawa: wana wa Siha, wana wa Hasufa, wana wa Tabaoti, wana wa Kerosi, wana wa Sia, wana wa Padoni, wana wa Lebana, wana wa Hagada, wana wa Salmai, wana wa Hanani, wana wa Gideli, wana wa Gahari, wana wa Raya, wana wa Resini, wana wa Nekoda, wana wa Gazamu, wana wa Uza, wana wa Pasea; wana wa Besai, wana wa Munimu, wana wa Nefisisimu, wana wa Bakibuki, wana wa Hakufa, wana wa Harihuri; wana wa Basiliti, wana wa Mehida, wana wa Harsa; wana wa Barkosi; wana wa Sisera, wana wa Tema; wana wa Nesia, wana wa Hatifa. Wana wa watumwa wa Salomo walikuwa hawa: wana wa Sotai, wana wa Sofereti, wana wa Perida, wana wa Yala, wana wa Darkoni, wana wa Gideli, wana wa Sefatia, wana wa Hatili, wana wa Pokereti-Hasebaimu, wana wa Amoni. Watumishi wa Nyumbani mwa Mungu na wana wa watumwa wake Salomo wote pamoja walikuwa 392. Nao hawa ndio waliopanda toka Teli-Mela, Teli-Harsa, Kerubu-Adoni na Imeri, lakini hawakuweza kuijulisha milango ya baba zao, wala vizazi vyao, kama ndio Waisiraeli: wana wa Delaya, wana wa Tobia, wana wa Nekoda; nao walikuwa watu 642. Tena kwao watambikaji: wana wa Habaya, wana wa Hakosi, wana wa Barzilai aliyechukua mmoja wao binti Barzilai wa Gileadi, awe mkewe, kwa hiyo aliitwa kwa jina lao. Hawa walikitafuta kitabu chao cha udugu wao, lakini hawakukiona, kwa hiyo wakakatazwa utambikaji. Mtawala nchi akawaambia: Msile kabisa vyakula vitokavyo Patakatifu Penyewe, mpaka atakapoondokea mtambikaji mwenye Urimu na Tumimu (Mwanga na Kweli). Huo mkutano wote pamoja walikuwa watu 42360, pasipo watumwa na vijakazi wao, nao walikuwa 7337; tena walikuwako waimbaji wa kiume na wa kike 245. Farasi wao walikuwa 736, nyumbu wao 245, ngamia 435, tena punda 6720. Wakuu wengine wa milango wakatoa vipaji vya kufanyia hizo kazi za jengo: mtawala nchi alitoa na kutia katika kilimbiko: vipande vya dhahabu vilivyoitwa Dariko 1000, ndio shilingi kama 40000, na vyano 50 na mavazi ya watambikaji 530. Nao wakuu wa milango wengine wakatoa na kutia katika kilimbiko cha jengo: vipande vya dhahabu vilivoitwa Dariko 20000, ndio shilingi kama 800000, na vipande vya fedha vilivyoitwa Mane 2200, ndio shilingi kama 440000. Nao watu wengine wakatoa Dariko za dhahabu 20000, ndio shilingi kama 800000, na Mane za fedha 2000, ndio shilingi kama 400000 na mavazi ya watambikaji 67. Kisha watambikaji na Walawi na walinda malango na waimbaji nao watu wengine na watumishi wa Nyumbani mwa Mungu nao Waisiraeli wote wakakaa katika miji yao. Mwezi wa saba ulipofika, wana wa Isiraeli walikuwamo bado mijini mwao. Ndipo, watu wote pia walipokusanyika kama mtu mmoja katika uwanja ulioko mbele ya lango la Maji, wakamwambia mwandishi Ezera, alete kitabu cha Maonyo ya Mose, Mungu aliyowaagiza Waisiraeli. Mtambikaji Ezera akayaleta Maonyo, akayaweka mbele ya huo mkutano, kwani walikuja waume kwa wake na wote walioweza kusikia na kutambua maana, ikawa siku ya kwanza ya mwezi wa saba. Pale penye uwanja ulioko mbele ya lango la Maji akawasomea yaliyomo kitabuni, akaanza asubuhi, akamaliza, jua lilipokuwa kichwani, wakawako waume na wake na watambuzi, nao watu wote pia, wakakisikiliza hicho kitabu cha Maonyo. Hapo mwandishi Ezera alikuwa akisimama juu ya ulingo wa miti, walioutengeneza kwa ajili ya hili jambo, kando yake kuumeni kwake wakasimama Matitia na Sema na Anaya na Uria na Hilkia na Masea, tena kushotoni kwake Pedaya na Misaeli na Malkia na Hasumu nao Hasibadana, Zakaria na Mesulamu. Ezera akakifunua kitabu machoni pao watu wote, kwa kuwa alikuwa juu kuliko watu wote, napo hapo, alipokifunua, watu wote wakainuka. Ezera akamtukuza Bwana aliye Mungu mkubwa, nao watu wakamwitikia: Amin! Amin! na kuiinua mikono yao; kisha wakainama, wakamwangukia Bwana na kuzielekeza nyuso chini. Kisha Yesua na Bani na Serebia, tena Yamini, Akubu, Sabutai, Hodia, Masea, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani, Pelaya na Walawi wakawatambulisha watu haya Maonyo, watu wakiwa wamesimama papo hapo. Wakawasomea katika kitabu cha Maonyo ya Mungu kwa sauti kuu na kuyaeleza vema; hivyo watu waliyatambua maana papo hapo, yaliposomwa. Ndipo, Nehemia aliyekuwa mtawala nchi na Ezera aliyekuwa mtambikaji na mwandishi nao Walawi waliowatambulisha watu maana walipowaambia watu: Siku hii ya leo ni siku takatifu ya Bwana Mungu wenu! Msiomboleze, wala msilie machozi! Kwani watu wote walilia machozi walipoyasikia maneno ya Maonyo. Akaendelea akiwaambia: Haya! Nendeni, mle vinono pamoja na kunywa vinywaji vitamu! Nao wakosao vya kujiandalia wapelekeeni magawio! Kwani siku ya leo ni siku takatifu ya Mungu wetu. Kwa hiyo msisikitike! Kwani kumfurahia Bwana ndiko kunakowapa nguvu. Walawi wakawatuliza watu wote mioyo wakiwaambia: Nyamazeni! Kwani siku hii ni takatifu, kwa hiyo msisikitike. Ndipo, watu wote walipokwenda, wale, wanywe, wapeleke magawio, wafanye sikukuu yenye furaha kubwa, kwa kuwa waliyatambua hayo maneno, waliyojulishwa. Siku ya pili wakuu wa milango ya watu wote na watambikaji na Walawi wakakusanyika kwa mwandishi Ezera, wajifundishe vema maneno ya Maonyo. Wakaona palipoandikwa katika Maonyo, ya kuwa Bwana alimwagiza Mose kuwaambia wana wa Isiraeli, penye sikukuu ya mwezi wa saba wakae katika vibanda, wapige mbiu na kutangaza po pote penye miji yao namo Yerusalemu kwamba: Tokeni kwenda milimani, mlete matawi ya michekele na makuti ya michikichi na matawi ya vihagilo na makuti ya mitende na matawi ya miti yo yote yenye majani mengi, mpate kujenga vibanda, kama ilivyoandikwa! Ndipo, watu walipotoka, wakaleta matawi, wakajijengea vibanda kila mtu juu darini kwake napo penye nyua zao napo penye ua wa Nyumba ya Mungu napo penye uwanja ulioko kwenye lango la Maji napo penye uwanja ulioko kwenye lango la Efuraimu. Hivyo mkutano wao wote waliorudi mafungoni kwenye kutekwa wakajijengea vibanda, wakakaa vibandani; kwani tangu siku za Yosua, mwana wa Nuni, mpaka siku hiyo wana wa Isiraeli hawakufanya hivyo, ikawa furaha kubwa sana. Wakasoma katika kitabu cha Maonyo ya Mungu siku kwa siku, tangu siku ya kwanza hata siku ya mwisho. Wakafanya sikukuu siku saba, lakini siku ya nane pakawa na kusanyiko kuu, kama ilivyopasa. Siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wana wa Isiraeli wakakusanyika wakifunga mfungo na kuvaa magunia na kujitia mchanga vichwani. Waliokuwa wa uzao wa Kiisiraeli wenyewe wakajitenga na wenzao wote wa kabila jingine, kisha wakasimama wakiyaungama makosa yao na maovu, baba zao waliyoyafanya. Wakainuka, wasimame hapohapo, walipokuwa, wakasoma katika kitabu cha Maonyo ya Bwana Mungu wao saa tatu, saa tatu nyingine wakaungama na kumwangukia Bwana Mungu wao. Kisha Yesua na Banai, Kadimieli, Sebania, Buni, Serebia, Bani na Kenani wakatokea wakisimama hapo juu, Walawi wanaposimama, wakamlilia Bwana Mungu wao kwa kupaza sauti sana. Kisha Walawi Yesua nao Kadimieli, Bani, Hasabunia, Serebia, Hodia, Sebania na Petaya wakawaambia: Inukeni, mtukuzeni Bwana aliye Mungu wenu tangu kale hata kale! Watu na walitukuze Jina lako tukufu lililo kuu kupita matukuzo yote na sifa zote. Bwana, wewe ndiwe peke yako; wewe uliziumba mbingu, hizo mbingu zilizoko juu kuliko mbingu zote na vikosi vyao vyote, hata nchi nayo yote yaliyoko, hata bahari nayo yote yaliyomo; wewe ndiwe unayewapa wao wote kuwa wenye uzima, navyo vikosi vya mbinguni hukuangukia. Bwana Mungu, wewe ndiwe uliyemchagua Aburamu, ukamtoa Uri kwao Wakasidi, ukampa jina la Aburahamu. Ulipouona moyo wake kuwa mwelekevu mbele yako, ukafanya agano naye la kumpa nchi za Wakanaani na za Wahiti na za Waamori na za Waperizi na za Wayebusi na za Wagirgasi, uwape wao wa uzao wake, ukalitimiza neno lako, kwani wewe ndiwe mwongofu. Ulipoyaona mateso ya baba zetu katika nchi ya Misri, ukavisikia vilio vyao kwenye bahari ya Ushami, ndipo, ulipotoa vielekezo na vioja kwake Farao na kwa watumishi wake wote na kwa watu wote wa nchi yake, kwani ulijua, ya kuwa waliwakorofisha, ukajipatia Jina, kama lilivyo hata leo hivi. Ukaitenganisha bahari mbele yao, wakapita pakavu baharini katikati, nao waliowakimbiza ukawatupa vilindini, kama jiwe linavyotupwa katika maji yenye nguvu. Ukawaongoza mchana kwa wingu jeusi, tena usiku kwa wingu lenye moto kuwamulikia hiyo njia, waliyoishika. Mlimani kwa Sinai ulishuka kusema nao toka mbinguni, ukawapa maamuzi yanyokayo na Maonyo ya kweli na maongozi na maagizo mema. Ukawajulisha siku yako takatifu ya kupumzikia, ukawaagiza magizo na maongozi na maonyo kinywani mwa mtumishi wako Mose. Ukawapa vyakula toka mbinguni vya kuzikomesha njaa zao, ukatoa maji miambani ya kuzikomesha kiu zao, ukawaambia, ya kama wataingia katika nchi hii, waichukue, iwe yao, kwa kuwa uliuinua mkono wako, kwamba utawapa. Lakini wao baba zetu wakajikuza, wakazishupaza kosi zao, hawakuyasikia maagizo yako. Wakakataa kabisa kusikia, hawakuvikumbuka vioja vyako, ulivyovifanya kwao, wakazishupaza kosi zao, kwa upingani wao wakajitakia mkuu, wapate kurudi utumwani mwao. Lakini wewe Mungu huwaondolea watu makoa, u mwenye utu na huruma, tena mwenye uvumilivu na upole mwingi, kwa hiyo hukuwaacha. Hata hapo, walipojitengenezea ndama ya dhahabu kwa kuziyeyusha na kusema: Huyu ndiye Mungu wako aliyekutoa Misri, waliposema masimango makuu, hapo napo hukuwaacha kule nyikani kwa huruma zako nyingi, wala wingu jeusi halikuondoka mchana kwao kuwaongoza njiani, wala wingu lenye moto halikuondoka usiku kuwamulikia hiyo njia, waliyoishika. Ukawapa nayo roho yako njema ya kuwaerevusha, tena hukuwanyima Mana zako vinywani mwao, ukawapa nayo maji ya kuzikomesha kiu zao. Ukawatunza vema miaka arobaini njiani, wasikose kitu; mavazi yao hayakuchakaa, wala miguu yao haikuvimba. Ukawapa nchi za kifalme pamoja na watu wao, ukawagawia nchi huko na huko, ziwe mafungu yao, wakaichukua nchi ya Sihoni na nchi ya mfalme wa Hesiboni na nchi ya Ogi, mfalme wa Basani. Ukazidisha wana wao kuwa wengi kama nyota za mbinguni, ukawaingiza katika nchi hii, uliyowaambia baba zao, ya kuwa wataiingia, iwe yao. Wana wao wakaiingia nchi hii, wakaichukua, iwe yao, ukawanyenyekeza wenyeji wa nchi hii mbele yao, wale Wakanaani, ukawatia mikononi mwao wafalme wao pamoja na watu wa nchi hii, wawafanyizie, kama walivyotaka. Wakateka miji yenye maboma na nchi yenye manono, wakachukua nyumba zilizojaa mema yote, ziwe zao, hata visima vilivyochimbuliwa miambani, nayo mizabibu na michekele na miti mingi ya matunda, wakala, wakashiba, wakanenepa, wakaufurahia wema wako ulio mkubwa. Lakini wakakataa kutii, wakakuinukia, wakayatupa Maonyo yako nyuma yao, nao wafumbuaji wako wakawaua, kwa kuwa waliwaumbua kwa ushuhuda wao, wawarudishe kwako, wakasema masimango makuu. Kwa hiyo ukawatoa na kuwatia mikononi mwao waliowasonga, wakawasonga kweli; lakini hizo siku za kusongeka kwao walipokulilia, ukawasikia toka mbinguni, tena kwa huruma zako nyingi ukawapatia waokozi, wakawaokoa mikononi mwao waliowasonga. Walipopata utulivu wakarudia kuyafanya yaliyo mabaya machoni pako, ukawaacha tena mikononi mwa adui zao, wawatawale. Lakini walipokulilia tena, ndipo, wewe ulipowasikia toka mbinguni, ukawaponya kwa huruma zako mara nyingi. Nawe ukawaumbua kwa ushuhuda wako, upate kuwarudisha, wayafuate Maonyo yako, lakini wao wakajikuza, hawakuyasikia maagizo yako, nayo maamuzi yako wakayakosea, tena mtu akiyafanya hujipatia kuishi. Wakakutolea mabega makatavu, nazo kosi zao wakazishupaza, hawakusikia. Lakini wewe ukawavumilia miaka mingi, ukawaumbua kwa ushuhuda wa Roho yako iliyowatokea vinywani mwa wafumbuaji wako, lakini hawakusikiliza; ndipo, ulipowatia mikononi mwao makabila ya nchi hizi. Lakini kwa huruma zako nyingi hukuwaangamiza kabisa, wala hukuwaacha, kwani wewe ndiwe Mungu mwenye utu na huruma. Sasa Mungu wetu uliye Mungu mkuu mwenye uwezo wa kutia woga, unashika maagano ya upole! Yasiwe madogo mbele yako masumbuko yote yaliyotupata sisi, wafalme wetu na wakuu wetu na watambikaji wetu na wafumbuaji wetu na baba zetu nao wote walio ukoo wako tangu hapo, wafalme wa Asuri walipotujia hata siku hii ya leo. Wewe u mwongofu katika hayo yote yaliyotujia, kwani ulifanya yaliyo kweli, lakini sisi tukafanya maovu. Nao wafalme wetu na wakuu wetu na watambikaji wetu na baba zetu hawakuyafanya Maonyo yako, masikio yao hawakuyategea maagizo yako wala ushuhuda wako, uliowashuhudia. Ijapo uliwapa ufalme wao, ukawatolea wema wako mwingi, ukawapa nchi kubwa yenye vinono, waione na macho yao, lakini wao hawakukutumikia, wala hawakurudi na kuyaacha matendo yao mabaya. Kwa hiyo sisi tu watumwa katika nchi, uliyowapa baba zetu, wayale mazao yake na mema yake, tazama, kuku huku sisi tu watumwa. Mapato yake mengi ni yao wafalme, uliotupa, watutawale kwa ajili ya makosa yetu, nao wanaitawala hata miili yetu na nyama wetu wa kufuga, kama inavyowapendeza. Kweli sisi tumo katika masongano makubwa. Kwa ajili ya haya yote sisi tunafanya agano la kweli, tunaliandika na kulitia muhuri ya wakubwa wetu na ya Walawi wetu na ya watambikaji wetu. Nao waliotia muhuri yao hi hawa: Mtawala nchi Nehemia, mwana wa Hakalia, na Sedekia; Seraya, Azaria, Yeremia; Pashuri, Amaria, Malkia; Hatusi, Sebania, Maluki; Harimu, Meremoti, Obadia; Danieli, Ginetoni, Baruku; Mesulamu, Abia, Miyamini; Mazia, Bilgai, Semaya; hawa ndio watambikaji. Nao Walawi ndio: Yesua, mwana wa Azania, Binui wa wana wa Henadadi, Kadimieli; na ndugu zao Sebania, Hodia, Kelita, Pelaya, Hanani; Mika, Rehobu, Hasabia; Zakuri, Serebia, Sebania; Hodia, Bani, Beninu. Wakuu wa watu ndio: Parosi, Pahati-Moabu, Elamu, Zatu, Bani; Buni, Azgadi, Bebai; Adonia, Bigwai, Adini; Ateri, Hizikia, Azuri; Hodia, Hasumu, Besai; Harifu, Anatoti, Nobai; Magipiasi, Mesulamu, Heziri; Mesezabeli, Sadoki, Yadua; Pelatia, Hanani, Anaya; Hosea, Hanania, Hasubu; Halohesi, Piliha, Sobeki; Rehumu, Hasabuna, Masea; na Ahia, Hanani, Anani; Maluki, Harimu, Baana. Nao watu wengine wote, watambikaji, Walawi, walinda malango, waimbaji, watumishi wa Nyumbani mwa Mungu, nao wote waliojitenga na watu wa makabila ya nchi hizi, wayashike Maonyo ya Mungu, wake zao na wana wao wa kiume na wa kike, wote pia waliojua kuitambua maana, wakawafuata ndugu zao watukufu wakijiapiza na kuapa kwamba: Tuendelee na kuyafuata Maonyo ya Mungu yaliyotolewa mkononi mwa Mose, mtumishi wake Mungu, tena tuyashike na kuyafanya maagizo yote na maamuzi yake na maongozi yake Bwana Mungu wetu. Tusiwape watu wa makabila ya nchi hii wana wetu wa kike, wala wana wa kike wa kwao tusiwachukue, tuwape wana wetu wa kiume, wala tusinunue cho chote kwao watu wa makabila ya nchi hii katika siku za mapumziko na katika siku takatifu, wakileta vyombo na vilaji kuviuza siku ya mapumziko. Tena kila mwaka wa saba tuache kulima, nayo madeni yo yote tuwaachilie watu. Tena wakajisimamisha na kujiagiza wenyewe kutoa kila mtu kwa mwaka thumuni tatu za msaada wa kazi za Nyumba ya Mungu, zilipe mikate, anayowekewa Bwana, navyo vipaji vya tambiko vya kila siku nazo ng'ombe za tambiko za kila siku na za siku za mapumziko, nazo za miandamo ya mwezi, nazo za sikukuu na za siku takatifu na za Mapoza, Waisiraeli wakijitafutia upozi kwa ajili ya makosa yao, kale na kale zilipe kazi zote za Nyumba ya Mungu wetu. Kisha sisi watambikaji na Walawi pamoja na watu wote tukaipigia kura michango ya kuni, watakazoipelekea Nyumba ya Mungu wetu milango kwa milango ya baba zetu mwaka kwa mwaka penye siku zilizowekwa, tupate kuziteketeza ng'ombe za tambiko mezani pa Bwana Mungu wetu, kama ilivyoandikwa katika Maonyo. Tena tukajisimamisha kuleta Nyumbani mwa Bwana malimbuko ya mashamba yetu na ya miti yote ya matunda mwaka kwa mwaka, nao wazaliwa wa kwanza wa wana wetu na wa nyama wetu wa kufuga, kama ilivyoandikwa katika Maonyo, ndiyo malimbuko ya ng'ombe wetu na ya mbuzi na kondoo wetu, tuyapeleke Nyumbani mwa Mungu wetu kuwapa watambikaji wanaotumikia Nyumbani mwa Mungu wetu. Tena tukajisimamisha kutoa malimbuko ya unga wetu wa kwanza wa kupika mikate na michango mingine itupasayo na matunda ya miti yote na mvinyo mbichi na mafuta, tuyapelekee watambikaji katika vyumba vyao vilivyopo penye Nyumba ya Mungu wetu, nao Walawi tuwapelekee mafungu ya kumi ya mashamba yetu, kwani Walawi ndio wanaoyatoza mafungu ya kumi katika miji yote, tunakolima. Tena Walawi wakiyatoza mafungu ya kumi, mtambikaji aliye mwana wa Haroni sharti awe pamoja na hao Walawi, Walawi wapeleke fungu la kumi la mafungu yao ya kumi vyumbani mwa nyumba ya vilimbiko. Kwani humo vyumbani ndimo, wana wa Isiraeli na wana wa Lawi watakamopeleka michango ya ngano na ya mvinyo mbichi na ya mafuta, kwani humo ndimo, vyombo vitakatifu vilimo, nao watambikaji na watumishi na walinda malango na waimbaji wamo mumo humo. Hatutaiacha Nyumba ya Mungu wetu, ikose cho chote. Wakuu wa watu wakaja kukaa Yerusalemu, lakini watu wengine wakapiga kura, katika kila watu kumi wapate mmoja wa kumpeleka kukaa Yerusalemu ulio mji mtakatifu; wale wengine tisa wakae mijini. Watu wakawabariki hao waume waliojipa mioyo ya kukaa Yerusalemu. Hawa ndio wakuu wa mitaa waliokaa Yerusalemu namo mijini mwa nchi ya Yuda; wakakaa kila mtu mahali palipokuwa mali yake katika miji yao: Waisiraeli, watambikaji, Walawi, watumishi wa Nyumbani mwa Mungu na wana wa watumwa wa Salomo. Yerusalemu wakakaa wengine wao wana wa Yuda na wana wa Benyamini. Wana wa Yuda walikuwa: Ataya, mwana wa uzia, mwana wa Zakaria, mwana wa Amaria, mwana wa Sefatia, mwana wa Mahalaleli wa wana wa Peresi. Na Masea, mwana wa Baruku, mwana wa Koli-Hoze, mwana wa Hazaya, mwana wa Adaya, mwana wa Yoyaribu, mwana wa Zakaria, mwana wa Msiloni. Wana wote wa Peresi waliokaa Yerusalemu walikuwa waume wenye nguvu 468. Hawa ndio wana wa Benyamini: Salu, mwana wa Mesulamu, mwana wa Yoedi, mwana wa Pedaya, mwana wa Kolaya, mwana wa Masea, mwana wa Itieli, mwana wa Yesaya, nyuma yake Gabai-Salai; ni watu 928. Yoeli, mwana wa Zikiri, alikuwa msimamizi wao, naye Yuda, mwana wa Hasenua, alikuwa msimamizi wa pili wa mji. Watambikaji walikuwa: Yedaya, mwana wa Yoyaribu, Yakini, Seraya, mwana wa Hilkia, mwana wa Mesulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayoti, mwana wa Ahitubu, aliyekuwa msimamizi mkuu wa Nyumba ya Mungu; pamoja na ndugu zao walioifanyia Nyumba ya Mungu kazi, walikuwa watu 822. Tena Adaya, mwana wa Yerohamu, mwana wa Pelalia, mwana wa Amusi, mwana wa Zakaria, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkia; pamoja na ndugu zake walio wakuu wa milango walikuwa watu 242. Tena Amasai, mwana wa Azareli, mwana wa Azai, mwana wa Mesilemoti, mwana wa Imeri; pamoja na ndugu zao waliokuwa wenye nguvu walikuwa watu 128; msimamizi wao alikuwa Zabudieli, mwana wa Hagedolimu. Walawi walikuwa: Semaya, mwana wa Hasubu, mwana wa Azirikamu, mwana wa Hasabia, mwana wa Buni, na Sabutai na Yozabadi waliokuwa wenye kazi za nje ya Nyumba ya Mungu, nao waliokuwa miongoni mwao wakuu wa Walawi. Tena Matania, mwana wa Mika, mwana wa Zabudi, mwana wa Asafu, kiongozi wao walioimba shangilio la kushukuru, watu walipoomba. Tena Bakibukia aliyekuwa miongoni mwa ndugu zake; tena abuda, mwana wa samua, mwana wa Galali, mwana wa Yedutuni. Walawi wote katika mji mtakatifu walikuwa watu 284. Walinda malango walikuwa: Akubu na Talmoni na ndugu zao; ndio walioyangoja malango, walikuwa watu 172. Waisiraeli wengine, nao watambikaji na Walawi wakakaa katika miji yote ya nchi ya Yuda, kila hapo palipokuwa fungu lake. Lakini watumishi wa Nyumbani mwa Mungu wakakaa Ofeli; Siha na Gisipa walikuwa wasimamizi wao watumishi wa Nyumbani mwa Mungu. Msimamizi wa Walawi mle Yerusalemu alikuwa Uzi, mwana wa Bani, mwana wa Hasabia, mwana wa Matania, mwana wa Mika wa wana wa Asafu waliokuwa waimbaji, akawasaidia kutumikia Nyumbani mwa Mungu. Kwani mfalme aliagiza kazi zao na mshahara wao hao waimbaji, ndio waupate siku kwa siku. Petaya, mwana wa Mesezabeli, wa wana wa zera, mwana wa Yuda, alikuwa amewekwa na mfalme kuyatengeneza mambo yote ya watu. Nako mashambani kwenye viwanja vya kale wakakaa Wayuda wengine Kiriati-Arba na katika vijiji vyake, tena Diboni na katika vijiji vyake na Yekabuseli na katika viwanja vyake, tena Yesua na Molada na Beti-Peleti, Hasari-Suali na Beri-Seba na katika vijiji vyake, Siklagi na Mekona na katika vijiji vyake, Eni-Rimoni na Sora na Yarmuti, Zanoa, Adulamu na katika viwanja vyao. Lakisi na mashambani kwake, Azeka na katika vijiji vyake; basi, wakatua toka Beri-Seba hata bonde la Hinomu. Lakini wana wa Benyamini wakakaa kuanzia Geba: Mikimasi na Aya na Beteli na katika vijiji vyake, Anatoti, Nobu, Anania, Hasori, Rama, Gitaimu, Hadidi, Seboimu, Nebalati, Lodi na Ono na Bondeni kwa Mafundi. Walawi wengine, ambao kwao kulikuwa kwa Wayuda, wakakaa kwa Wabenyamini. Hawa ndio watambikaji na Walawi waliorudi milimani kwao pamoja na Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na Yesua: Seraya, Yeremia, Ezera, Amaria, Maluki, Hatusi, Sekania, Rehumu, Meremoti, Ido, Ginetoi, Abia, Miyamini, Madia, Bilga, Semaya, Yoyaribu, Yedaya, Salu, Amoki, Hilkia, Yedaya; hawa walikuwa wakuu wa watambikaji na wa ndugu zao katika siku za Yesua. Walawi walikuwa: Yesua, Binui, Kadimieli, Serebia, Yuda, Matania; yeye na ndugu zake waliongoza nyimbo za kushukuru; ndugu zao Bakibukia na Uni wakasimama usoni pao, wawasaidie. Yesua akamzaa Yoyakimu, Yoyakimu akamzaa Eliasibu, Elaisibu akamzaa Yoyada, Yoyada akamzaa Yonatani, Yonatani akamzaa Yadua. Watambikaji waliokuwa wakuu wa milango wiku za Yoyakimu ndio hawa: Meraya wa mlango wa Seraya, Hanania wa mlango wa Yeremia, Mesulamu wa mlango wa Ezera, Yohana wa mlango wa Amaria, Yonatani wa mlango wa Meluki, Yosefu wa mlango wa Sebania, Adina wa mlango wa Harimu, Helkai wa mlango wa Merayoti, Zakaria wa mlango wa Ido, Mesulamu wa mlango wa Ginetoni, Zikiri wa mlango wa Abia, Piltai wa mlango wa Minyamini na wa Moadia, Samua wa mlango wa Bilga, Yonatani wa mlango wa Semaya, Matinai wa mlango wa Yoyaribu, Uzi wa mlango wa Yedaya, Kalai wa mlango wa Salai, Eberi wa mlango wa Amoki, Hasabia wa mlango wa Hilkia, Netaneli wa mlango wa Yedaya. Walawi waliokuwa wakuu wa milango waliandikwa siku za Eliasibu, Yoyada na Yohana na Yadua; lakini watambikaji waliandikwa, Mpersia Dario aliposhika ufalme. Wana wa Lawi waliokuwa wakuu wa milango waliandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za kale kufikisha siku za Yohana, mwana wa Eliasibu. Nao wakuu wa Walawi ni hawa: Hasabia, Serebia na Yesua, mwana wa Kadimieli, nao ndugu zao waliosimama usoni pao, wawasaidie kuimba mashangilio ya kushukuru, kama Dawidi aliyekuwa mtu wa Mungu alivyoagiza, wapokeane zamu kwa zamu. Matania na Bakibukia, Obadia, Mesulamu, Talmoni na Akubu walikuwa walinda malango, wakavilinda vilimbiko vilivyomo vyumbani penye malango. Hawa ndio waliokuwako siku za Yoyakimu, mwana wa Yesua, mwana wa Yosadaki, na siku za mtawala nchi Nehemia na za Ezera aliyekuwa mtambikaji na mwandishi. Walipotaka kulieua boma la Yerusalemu wakawatafuta Walawi mahali pao po pote, wawapeleke Yerusalemu kufanya mweuo na furaha kwa kushukuru na kuimbia matoazi na mapango na mazeze. Wakakusanyika wana wao walio waimbaji wakitoka katika nchi iliyouzunguka Yerusalemu na viwanjani kwa Netofa na Beti-Gilgali na mashambani kwenye Geba na Azimaweti; kwani kwenye vile viwanja ndiko, waimbaji walikojijengea kuzunguka Yerusalemu. Watambikaji na Walawi walipokwisha kujitakasa, wakawatakasa watu na malango na boma. Kisha nikawapeleka wakuu wa Yuda bomani juu, nikasimama hapo na makundi mawili makubwa ya kushukuru, moja likaenda ukutani juu kufika penye lango la Jaani. Nyuma yao wakafuata Hosaya na nusu ya wakuu wa Yuda: Azaria, Ezera na Mesulamu, Yuda na Benyamini na Semaya na Yeremia. Nao wana wa watambikaji wengine walikuwako wenye matarumbeta: Zakaria, mwana wa Yonatani, mwana wa Semaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu, na ndugu zake: Semaya na Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Netaneli na Yuda na Hanani wakishika vyombo vya kuimbia vya Dawidi aliyekuwa mtu wa Mungu, naye mwandishi Ezera akawatangulia. Wakaja kulifikia lango la Jicho la Maji, wakaenda moja kwa moja wakaipanda ngazi ya mji wa Dawidi, wakaendelea kupanda, hata wakafika ukutani juu penye nyumba ya Dawidi mpaka kwenye lango la Maji lililoko upande wa maawioni kwa jua. Lakini kundi la pili la kushukuru likashika njia ya upande mwingine, nami nikawafuata na nusu ya watu, tukienda ukutani juu, tukaupita mnara wa Tanuru, tukaufikia ukuta mpana, kisha tukapita juu penye lango la Efuraimu vilevile penye lango la Mji wa Kale na penye lango la Samaki, tukaupita mnara wa Hananeli na mnara wa Mea, tukalifikia lango la Kondoo, wakasimama penye lango la Kifungoni. Kisha makundi yote mawili ya kushukuru wakajisimamisha penye Nyumba ya Mungu pamoja na mimi na nusu ya watawalaji. Ndipo, yalipolia matarumbeta ya watambikaji Eliakimu, Masea, Minyamini, Mikaya, Eliyoenai, Zakaria na Hanania. Nao Masea na Semaya na Elazari na Uzi na Yohana na Malkia na Elamu na Ezeri waliokuwa waimbaji wakaimba wakiongozwa na Iziraya. Kisha siku hiyo wakatoa ng'ombe nyingi za tambiko, wakafurahi, kwa kuwa Mungu amewafurahisha na kuwapatia furaha kubwa, hata wanawake na watoto wakafurahi, mashangilio ya furaha hiyo ya Yerusalemu yakasikilika hata mbali. Siku hiyo wakawekwa watu wa kuviangalia vyumba vya vilimbiko na michango na malimbuko na mafungu ya kumi, wayakusanye mashambani kwenye miji yote, watu waliyoagizwa na Maonyo kuwatolea watambikaji na Walawi, kisha wayaweke humo, kwani Wayuda waliwafurahia watambikaji na Walawi kwamba: Wanasimama kazini. Nao wakalinda ulinzi wa Mungu wao na ulinzi wa matakaso, nao waimbaji na walinda malango wakazishika zamu zao, kama Dawidi na mwanawe Salomo walivyoviagiza. Kwani nazo hizo siku za kale za Dawidi na za Asafu walikuwako wakuu wa waimbaji na nyimbo za kumshangilia na za kumshukuru Mungu. Siku za Zerubabeli na za Nehemia Waisiraeli wote walitoa mafungufungu ya kuwapa waimbaji na walinda malango siku kwa siku yaliyowapasa. Hivyo vipaji wakavitakasa, kisha wakawapa Walawi, nao Walawi walipokwisha kuvitakasa wakatoa humo vya kuwapa wana wa Haroni. Siku hiyo, watu waliposomewa masikioni pao yaliyoandikwa katika kitabu cha Maonyo, pakaoneka palipoandikwa kwamba: Kale na kale asije Mwamoni wala Mmoabu kuuingia mkutano wa Mungu! Kwani kale hawakuwajia Waisiraeli na kuwagawia chakula na maji, ila walimpenyezea Bileamu mali, aje kuwaapiza, lakini Mungu alikigeuza hicho kiapizo kuwa mbaraka. Kwa hiyo walipoyasikia Maonyo wakawatenga kwao Waisiraeli wote pia waliochanganyika nao. Hayo yalipokuwa hayajafanyika bado, mtambikaji Eliasibu alikuwa amewekwa kuviangalia vyumba vya Nyumba ya Mungu. Naye kwa kuwa ndugu yake Tobia alimpa chumba kikubwa; ndimo, walimoweka kale vilaji vya tambiko, uvumba na vyombo na mafungu ya kumi: ngano, mvinyo mbichi na mafuta, watu waliyoagizwa kuwapa Walawi, waimbaji na walinda malango, nayo michango ya watambikaji. Hayo yote yalipofanyika, mimi nilikuwa simo Yerusalemu, kwani katika mwaka wa thelathini na mbili wa Artasasta, mfalme wa Babeli, nalikwenda kwake mfalme; siku zilipopita, nikamwomba mfalme ruhusa. Nilipokuja Yerusalemu nikayatambua hayo mabaya, Eliasibu aliyoyafanya kwa ajili yake Tobia akimpa chumba uani penye Nyumba ya Mungu. Nikakasirika sana, nikavitoa vyombo vyote vya nyumbani mwa Tobia mle chumbani, nikavitupa nje, nikaagiza, wavitakase hivyo vyumba, kisha nikarudisha humo vyombo vya Nyumba ya Mungu na vilaji vya tambiko na uvumba. Nikajulishwa, ya kuwa Walawi hawakupewa mafungu yao yawapasayo; kwa hiyo Walawi na waimbaji waliofanya kazi za Mungu walikuwa wamekimbilia kila mtu shamba lake. Ndipo, nilipowagombeza watawalaji na kuwauliza: Mbona Nyumba ya Mungu imeachwa hivyo? Nikawakusanya, nikawaweka tena mahali pao pa utumishi. Wayuda wote walipoyaleta tena mafungu ya kumi: ngano na mvinyo mbichi na mafuta na kuyaweka penye vilimbiko, nikaweka watunza vilimbiko, waviangalie hivyo vilimbiko, ndio mtambikaji Selemia na mwandishi Sadoki na Pedaya aliyekuwa Mlawi naye, tena Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania, kuwa msaidiaji wao, kwani hawa waliwaziwa kuwa welekevu, kisha ikawa kazi yao kuwagawia ndugu zao mafungu yao. Mungu wangu unikumbukie haya, wala usiyafute matendo ya upole wangu, niliyoitendea Nyumba ya Mungu wangu, kazi zake ziangaliwe vema! Siku hizo nikaona katika nchi ya Yuda, ya kuwa wako wanaokanyaga makamulio siku ya mapumziko, ya kuwa wengine hupeleka machungu ya ngano chanjani kwa kuchukuza punda, wakawatwika hata mvinyo, zabibu, kuyu na mizigo yo yote, wakaipeleka Yerusalemu siku ya mapumziko. Ndipo, nilipowaonya hiyo siku, walipouza vilaji. Nao Watiro waliokaa huku wakaleta samaki na vingine vyo vyote vya kuuza, wakaviuzia wana wa Yuda namo mle Yerusalemu siku ya mapumziko. Nikawagombeza wakuu wa miji ya Yuda na kuwaambia: Hili ni neno baya zaidi, mnalolifanya siku ya mapumziko. Je? Baba zenu hawakuyafanya yayo hayo? Hii siyo sababu, Mungu wetu akituletea haya mabaya sisi na mji huu? Kumbe ninyi mwataka kuwapatia Waisiraeli makali yenye moto yaliyo makubwa zaidi, mkiichafua siku ya mapumziko! Ndipo, nilipoagiza, milango ifungwe, giza lilipoanza kuingia penye malango ya Yerusalemu siku ya kuiandalia siku ya mapumziko, kisha mikaagiza, isifunguliwa hata siku ifuatayo, ndiyo ya mapumziko, nikachukua vijana wa kwangu, nikawasimamisha malangoni kuangalia, usiingie mzigo wo wote siku ya mapumziko. Kwa hiyo wachuuzi na wauzaji wa vitu vyo vyote hawakuwa na budi kulala nje ya Yerusalemu mara moja, hata mara mbili. Nikawaonya na kuwaambia: Mbona mnalala mbele ya ukuta? Mkivifanya tena, nitawakamata na kuwafunga. Tangu hapo hawakuja tena siku ya mapumziko. Kisha nikawaambia Walawi, wajitakase, kisha waje kiyalinda malango, waitakase siku ya mapumziko. Mungu wangu, haya nayo unikumbukie, kanihurumie kwa upole wako mwingi! Tena nikaona siku hizo, ya kuwa wako Wayuda waliooa wake wa Waasdodi na wa Waamoni na wa Wamoabu. Nao wana wao nusu wakasema Kiasdodi, hawakuweza kusema Kiyuda, ila walisema misemo yao hawa na hawa. Nikawagombeza na kuwaapiza na kuwapiga, waume wengine nikawavuta nywele. Kisha nikawaapisha na kumtaja Mungu kwamba: Msiwaoze wana wao wana wenu wa kike, wala msichukue kwao wana wa kike, mwape wana wenu wa kiume au mwaoe wenyewe! Je? Siyo haya, Salomo, mfalme wa Isiraeli, aliyoyakosa? Katika mataifa mengi hakuwako mfalme kama yeye, naye alikuwa amependwa na Mungu wake, kwa hiyo Mungu akampa kuwa mfalme wa Waisiraeli wote; lakini naye yeye wanawake wageni wakamkosesha. Tunasikiaje kwenu, ya kuwa mnayafanya hayo mabaya yote yaliyo makubwa, mkiyavunja maagano, tuliyoyafanya na Mungu wetu, kwa kuoa wanawake wageni? Mmoja wao wana wa mtambikaji mkuu Yoyada, mwana wa Eliasibu, alikuwa amemwoa binti Mhoroni sanibalati; huyu nikamfukuza, asikae kwangu. Mungu wangu, wakumbukie hivyo, walivyouchafua utambikaji kwa kuyavunja maagano ya utambikaji na ya Walawi! Ndivyo, nilivyowaeua na kuyaondoa mambo yote ya kigeni, nikawasimikia watambikaji na Walawi zamu zao za utumishi wa kila mtu katika kazi yake. Nikayatengeneza nayo matoleo ya kuni na ya malimbuko, yafanyike siku zizo hizo zilizowekwa. Mungu wangu, nikumbukie haya, unipatie mema! Ahaswerosi alikuwa akitawala majimbo 127 kutoka nchi ya Uhindi mpaka nchi ya Nubi. Ikawa katika siku zake Ahaswerosi hapo, yeye mfalme Ahaswerosi alipokaa katika kiti chake cha kifalme jumbani mwake huko Susani, katika mwaka wa tatu wa ufalme wake ndipo, alipowafanyia wakuu wake wote pamoja na watumishi wake karamu kubwa. Wakawako mbele yake wakuu wa vikosi vya Persia nao vya Media, hata wenye macheo na wakuu wa majimbo. Akawaonyesha mali na malimbiko ya ufalme wake nayo marembo na utukufu wake mwingi siku nyingi, yaani siku 180. Siku hizo zilipokwisha kupita, mfalme akawafanyia watu wote pia waliopatikana mle Susani penye jumba lake, wakubwa kwa wadogo, karamu ya siku saba uani penye bustani ya jumba la mfalme. Mazulia meupe na meusi mazuri mno yalikuwa yamefungwa kwa kamba za pamba nyeupe na nyekundu katika pete za fedha penye nguzo za mawe meupe. Nayo magodoro ya kukalia yaliyofumwa kwa nyuzi za dhahabu na za fedha yalikuwa yametandikwa sakafuni palipotengenezwa kwa mawe mekundu na meupe na ya manjano na meusi. Vyombo, watu walivyovipata vya kunywea, vilikuwa vya dhahabu; hivyo vyombo navyo vilipitanapitana kwa namna zao, nazo mvinyo za kifalme zilikuwa nyingi, kama inavyoupasa utu wa mfalme. Kama ilivyoagizwa, watu wakanywa, kama walivyotaka pasipo kushurutishwa; kwani nidvyo, mfalme alivyowaagiza wakuu wote wa nyumbani mwake, waache, kila mtu anywe, kama anavyopendezwa. Naye Wasti, mkewe mfalme, alifanya karamu ya wanawake mle ndani ya jumba la kifalme la mfalme Ahaswerosi. Siku ya saba, moyo wa mfalme ulipochangamshwa na mvinyo, akawaambia akina Mehumani, Bizita, Harbona, Bigita, Abagita, zetari, na Karkasi, watumishi wake saba wa nyumbani waliomtumikia mfalme Ahaswerosi mwenyewe, wamlete Wasti mkewe mfalme, amtokee mfalme na kuvaa kilemba cha kifalme, awaonyeshe watu wote nao wakuu uzuri wake, kwani alikuwa kweli mwenye sura nzuri. Lakini Wasti, mkewe mfalme, akakataa kuja kwa ile amri, mfalme aliyompelekea kwa vinywa vya wale watumishi wa nyumbani. Ndipo, mfalme alipokasirika sana, makali yake yakawaka moto moyoni mwake. Basi, mfalme akafanya shauri na mafundi wa kuvijua vielekezo vya siku, kwani ilikuwa desturi yake mfalme kuulizana nao wote waliozijua amri na hukumu za serikali. Waliomfuata kwa ukuu walikuwa Karsina, Setari, Adimata, Tarsisi, Meresi, Marsina na Memukani, ndio wakuu saba wa Persia na wa Media waliotokea usoni pa mfalme, nao walikuwa wa kwanza katika ufalme huo. Akawauliza: Ndio nini inayopasa kwa amri za serikali kumfanyizia wasti, mkewe mfalme, kwa kuwa hakuifanya amri ya mfalme Ahaswerosi, aliyompelekea kwa vinywa vya wale watumishi wa nyumbani? Memukani akasema mbele ya mfalme na mbele ya hao wakuu: Siye mfalme peke yake, Wasti, mkewe mfalme, aliyemkosea, ila amewakosea nao wakuu wote na watu wote pia walioko katika majimbo ya mfalme Ahaswerosi. Kwani jambo hili la mkewe mfalme litatoka, lifike kwa wanawake wote, liwabeue bwana zao machoni pao, maana watasema: Mfalme Ahaswerosi aliagiza kumleta Wasti, mkewe mfalme, aje usoni pake, naye hakuja. Leo hivi wake wakuu wa Wapersia na wa Wamedia waliolisikia hilo jambo la mkewe mfalme watalisimulia wakuu wote wa mfalme; ndipo, yatakapokuwa mabezo na mateto ya kutosha. Mfalme akiyaona kuwa mema, na kutoke kwake amri ya kifalme, iandikwe katika amri za Wapersia na za Wamedia, isitanguke tena, kwamba: Wasti asitokee tena usoni pa mfalme Ahaswerosi, nao utukufu wake wa kifalme mfalme na ampe mwenzake aliye mwema kuliko yey. Mbiu hiyo, mfalme atakayoitoa, itakapotangazwa katika ufalme wake wote ulio mkubwa, ndipo, wanawake wote watakapowapa bwana zao macheo, wakubwa kwa wadogo. Neno hili mfalme na wakuu wakaliona kuwa jema, mfalme akafanya, kama Memukani alivyosema. Akatuma barua katika majimbo yote ya mfalme, kwa kila jimbo katika maandiko yao na kwa kila kabila katika msemo wa kwao kwamba: Kila mume sharti awe mkuu nyumbani mwake, akate mashauri, kama yanavyosemwa kwao. Baada ya mambo hayo, makali ya mfalme Ahaswerosi yalipotulia, akamkumbuka Wasti nayo, aliyoyafanya, nalo shauri, alilokatiwa. Ndipo, vijana wa mfalme waliomtumikia waliposema: Watu na wamtafutie mfalme vijana wa kike, walio wanawali wenye sura nzuri! Mfalme na aweke wasimamizi katika majimbo yote ya ufalme wake, wawakusanye vijana wa kike wote walio wanawali wenye sura nzuri, wawapeleke Susani jumbani mwa mfalme na kuwatia chumbani mwa wanawake mkononi mwake Hegai aliye mtumishi wa mfalme wa nyumbani wa kuwaangalia wanawake, kisha wapewe vyombo vyao vya kutengenezea uzuri. Naye kijana atakayempendeza mfalme na awe mkewe mfalme mahali pa wasti. Neno hili likampendeza mfalme, akafanya hivyo. Mle Susani, mlimokuwa wa jumba la mfalme, mlikuwa na mtu wa Kiyuda, jina lake Mordekai, mwana wa Yairi, mwana wa Simei, mwana wa Kisi, wa mlango wa Benyamini. Alitekwa Yerusalemu, akahamishwa pamoja na mateka waliohamishwa pamoja na Yekonia, mfalme wa Yuda; naye aliyewahamisha alikuwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli. Yule alikuwa akimlea Hadasa (Kihagilo), ndiye Esteri (Nyota), binti wa mjomba wake, kwa sababu hakuwa na baba wala na mama. Huyu kijana wa kike alikuwa mwenye uso upendezao na mwenye mwili mzuri. Baba yake na mama yake walipokufa, Mordekai alimchukua, awe mwanawe. Ikawa, agizo la mfalme, aliloliamrisha, lilipotangazwa, vijana wengi wa kike wakakusanywa Susani, mlimokuwa na jumba la mfalme, wakatiwa mkononi mwake Hegai; ndipo, Esteri naye alipochukuliwa na kupelekwa nyumbani mwa mfalme, akatiwa mikononi mwa Hegai aliyewaangalia wanawake. Akamwona kijana huyu kuwa mzuri, akampendeza sana, kwa hiyo akajihimiza kumpa vyombo vyake vya kutengenezea uzuri na posho yake; kisha akampa vijana wa kike saba waliochaguliwa nyumbani mwa mfalme, akamkalisha pamoja na hao vijana wake nyumbani mwa wanawake katika chumba kilichokuwa kizuri zaidi. Lakini Esteri kakuujulisha ukoo wake wala mlango wake, kwa kuwa Mordekai alimkataza, asiujulishe. Naye Mordekai akatembea siku kwa siku mbele ya ua wa nyumba ya wanawake, ajue, kama Esteri hajambo, tena ayajue nayo yatakayompata. Siku zilipotimia, hao vijana wakapelekwa mmoja mmoja kwa mfalme Ahaswerosi; vikafanyika, walipokwisha kukaa huko miezi kumi na miwili na kuyafuata maongozi ya wanawake. Kwani hapo ndipo, zilipotimia siku za kutakaswa kwao: miezi sita walipakwa kwa mafuta ya manemane, miezi sita mingine kwa manukato mengine, wanawake waliyoyatumia ya kutengenezea uzuri. Basi, hayo yalipokwisha, kila mara kijana alipoingia kwa mfalme hupewa yote, aliyoyataka kwenda nayo kutoka mle nyumbani mwa wanawake kuingia nyumbani mwa mfalme. Huenda jioni, tena hurudi asubuhi kukaa katika nyumba ya pili ya wanawake mkononi mwa Sasagazi, mtumishi wa nyumbani mwa mfalme aliyewaangalia masuria; haingii tena kwa mfalme, isipokuwa mfalme amependezwa naye, akaagiza, aitwe kwa jina lake. Basi, ikatimia hata siku yake Esteri, mwana wa Abihaili, mjomba wake Mordekai aliyemchukua, awe mwanawe. Alipoingia kwa mfalme hakutaka kitu, ni vile tu, Hegai, mtumishi wa nyumbani mwa mfalme aliyewaangalia wanawake, alivyomwambia, aende navyo. Naye Esteri alikuwa anawapendeza wote waliomwona kwa macho yao. Huyu Esteri akapelekwa kwa mfalme Ahaswerosi nyumbani mwake mwa kifalme katika mwezi wa kumi, ndio mwezi wa Tebeti katika mwaka wa saba wa kutawala kwake. Mfalme akampenda Esteri kuliko wanawake wote, kwani aliona upendeleo na utu mbele yake kuliko wanawali wote, akamvika kilemba cha kifalme kichwani pake, akamweka kuwa mkewe mahali pa Wasti. Kisha mfalme akawafanyizia wakuu na watumishi wake wote karamu kubwa, ndio karamu ya Esteri. Tena akayapunguzia majimbo yake kodi, nao watu akawapa matunzo, kama inavyompasa mfalme. Walipokusanywa wanawali mara ya pili, Mordekai alikuwa akikaa langoni pa mfalme. Lakini Esteri alikuwa hajaujulisha mlango wake wala ukoo wake, kama Mordekai alivyomwagiza; kwani Esteri aliyafanya maagizo yake Mordekai kama hapo, alipomlea. Siku zile, Mordekai alipokaa langoni pa mfalme, watumishi wawili wa mfalme wa nyumbani waliokuwa walinda mlango, ndio Bigitana na Teresi, wakakasirika sana, wakatafuta njia ya kumwua mfalme Ahaswerosi kwa mikono yao. Mordekai akapata kulijua shauri hilo, akamsimulia Esteri, mkewe mfalme, naye Esteri akamwambia mfalme katika jina la Mordekai. Kisha shauri hilo likanyatiwa, hata likavumbulikana, nao wale wawili wakatundikwa katika mti. Mambo haya yakaandikwa katika kitabu cha mambo ya siku machoni pa mfalme. Baada ya mambo hayo mfalme Ahaswerosi akampa Hamani, mwana wa Hamedata wa Agagi, kuwa mkuu akimwinua na kukiweka kiti cha ukuu wake juu zaidi kuliko vyao wakuu wote waliokuwa naye. Kwa hiyo watumishi wote wa mfalme waliokuwako kule langoni kwa mfalme wakampigia Hamani magoti na kumwangukia, kwani hivyo ndivyo, mfalme alivyoagiza kwa ajili yake. Lakini Mordekai hakumpigia magoti, wala hakumwangukia. Watumishi wa mfalme waliokuwako langoni kule kwa mfalme wakamwuliza Mordekai: Mbona unaikosea amri ya mfalme? Ikawa, walipomwambia haya siku kwa siku, asiwasikie, basi, wakamsimulia Hamani, waone, kama maneno ya Mordekai yataweza kusimama, kwani aliwaambia, ya kuwa yeye ni Myuda. Hamani alipoona, ya kuwa Mordekai hampigii magoti, wala hamwangukii, ndipo, makali yenye moto yalipomjaa Hamani moyoni. Lakini akaona, ya kama haimpasi kumkamata Mordekai peke yake, kwani walimwambia nao ukoo wake Mordekai; kwa hiyo Hamani akatafuta njia ya kuwaangamiza Wayuda wote pia waliokuwa katika ufalme wote wa Ahaswerosi, kwa kuwa ukoo wake Mordekai. Katika mwezi wa kwanza, ndio Nisani, katika mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahaswerosi wakapiga Puri, ndio kura, machoni pake Hamani siku kwa siku, hata mwezi kwa mwezi mpaka mwezi wa kumi na mbili, ndio Adari. Kisha Hamani akamwambia mfalme Ahaswerosi: Liko kabila moja lililotawanyika katikati ya makabila mengine katika majimbo yote ya ufalme wako, nao wanakaa na kujitenga kabisa, nayo maongozi yao ni mengine kabisa, siyo ya makabila yote mengine, nayo maagizo ya mfalme hawayafanyi. Kwa hiyo haimpasi mfalme kuwaacha, wajikalie tu. Ikiwa, mfalme avione kuwa vema, na viandikwe kwamba: Watu na wawaangamize! Kisha mimi nitawapimia wenye kazi hiyo mikononi mwao mizigo ya fedha elfu kumi, waipeleke na kuitia katika malimbiko ya mfalme. Ndipo, mfalme alipoitoa pete yake yenye muhuri kidoleni pake, akampa Hamani, mwana wa Hamedata wa Agagi, aliyekuwa mpingani wao Wayuda. Mfalme akamwambia Hamani: Zile fedha umepewa kukaa nazo, nao watu wa ule ukoo uwafanyizie yaliyo mema machoni pako. Kisha waandishi wa mfalme wakaitwa katika mwezi wa kwanza siku ya kumi na tatu; yote, Hamani aliyoyaagiza, yakaandikwa baruani kwa watawala nchi wa mfalme na kwa wenye amri wa kila jimbo moja na kwa wakuu wa kila kabila moja, kwa kila jimbo katika maandiko yao na kwa kila kabila katika msemo wa kwao. Hizo barua zikaandikwa katika jina la mfalme Ahaswerosi, zikatiwa muhuri kwa ile pete ya mfalme yenye muhuri, kisha zikapewa wapiga mbio, wazipeleke katika majimbo yote ya mfalme kwamba: Siku hiyo moja ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, Wayuda wote pia, vijana na wazee, wachanga na wanawake, watoweshwe kwa kuuawa na kwa kuangamizwa, nazo mali zao zitekwe. Mwandiko wa pili wa hizo barua ukatangazwa katika kila jimbo moja kuwa amri iliyotolewa na mfalme, watu wote pia wakaelezwa vema, wapate kuwa tayari siku hiyo. Wapiga mbio wakatoka upesi kwa lile neno la mfalme. Namo mjini mwa Susani, mlimokuwa na jumba la mfalme, ile amri ya mfalme ikatangazwa. Kisha mfalme na Hamani wakakaa, wanywe, lakini mji wa Susani ukawa umevurugika. Mordekai alipoyajua hayo yote yaliyofanyika, Mordekai akazirarua nguo zake, akavaa gunia na majivu, akatokea mjini katikati, akaomboleza maombolezo makuu yenye uchungu. Hivyo akaja mpaka hapo penye lango la mfalme, kwani mtu aliyevaa gunia hakuwa na ruhusa ya kuingia langoni kwa mfalme. Katika kila jimbo moja mahali po pote lile neno la mfalme lilipotangazwa, masikitiko makubwa yakawapata Wayuda, wakafunga mifungo pamoja na kulia machozi na kuomboleza; wengi wakakjitandikia magunia na majivu ya kuyalalia. Vijana wa kike wa Esteri na watumishi wake wa nyumbani walipokuja kumsimulia mambo hayo, mke wa mfalme akaumia sana moyoni, akatuma nguo kwake Mordekai, azivae na kuliondoa gunia lake, lakini hakukubali. Ndipo, Esteri alipomwita Hataki, ni mmoja wao watumishi wa nyumbani, mfalme aliowatoa wa kuwa naye, akamwagiza kumwuliza Mordekai, amjulishe sababu na maana ya mambo hayo. Hataki akatoka, akamkuta Mordekai uwanjani mjini langoni kwa mfalme. Mordekai akamsimulia yote yaliyompata, hata hesabu ya fedha, Hamani alizozisema kwamba atazipima, azitie katika malimbiko ya mfalme, atakapowaangamiza Wayuda. Kisha akampa karatasi iliyoandikwa ile mbiu iliyotangazwa Susani ya kuwatowesha, amwonyeshe Esteri na kumsimulia yote, kisha amwagize kwenda kwa mfalme kumlalamikia na kuuombea ukoo wake kwake. Hataki akaja, akamsimulia Esteri maneno ya Mordekai. Esteri naye akamwambia Hataki na kumwagiza, amwambie Mordekai: Watumishi wote wa mfalme na watu wote wa majimbo ya mfalme wanayajua haya: kila mtu, kama ni mwanamume au mwanamke aingiaye kwa mfalme katika ua wa ndani, asipokuwa ameitwa, hana budi kuuawa kwa ile amri moja ya mfalme; atakayepona ni yule tu, mfalme ampungiaye kwa bakora yake ya dhahabu. Nami sikuitwa kuingia kwa mfalme, sasa ni siku thelathini. Walipomsimulia Mordekai haya maneno ya Esteri. Mordekai akaagiza kumrudishia Esteri jibu la kwamba: Usijiwazie, ya kuwa kwa kukaa jumbani mwa mfalme utapona peke yako katika Wayuda wote. Lakini ukitaka kunyamaza kimya katika siku kama hizi, wokovu wa kuwaponya Wayuda utatoka mahali pengine, lakini wewe na mlango wa baba yako utaangamia; labda ni kwa ajili ya siku kama hizi, ukiwa mkewe mfalme. Esteri akaagiza kumrudishia Mordekai jibu la kwamba: Nenda, uwakusanye Wayuda wote wanaopatikana humu Susani! Kisha mfunge mfungo kwa ajili yangu mimi na kuniombea, msile, wala msinywe siku tatu usiku na mchana! Mimi nami nitafunga hivyo pamoja na vijana wangu wa kike, kisha nitaingia kwake mfalme, ingawa ni mwiko. Kama ni kuangamia, basi, na niangamie! Ndipo, Mordekai alipokwenda zake, akafanya yote, kama Esteri alivyomwagiza. Ikawa siku ya tatu, Esteri akavaa mavazi ya kifalme, akaja kusimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme. Naye mfalme alikuwa amekaa katika kiti chake cha kifalme nyumbani mwake mwa kifalme, akajielekeza kuutazama mlango wa hiyo nyumba. Ikawa, mfalme alipomwona Esteri, mkewe mfalme, akisimama uani, akaona upendeleo mbele yake, mfalme akampungia Esteri kwa bakora yake ya dhahabu iliyokuwa mkononi mwake. Ndipo, Esteri alipokuja kuugusa upembe wa hiyo bakora. Mfalme akamwuliza: Una shauri gani, Esteri, mkewe mfalme? Unataka nini? Ingawa ni nusu ya ufalme, utapewa. Esteri akamjibu: Kama ni vizuri kwake mfalme, mfalme na aje leo pamoja na Hamani kula karamu, Esteri aliyomfanyizia. Mfalme akaagiza: Mwiteni Hamani, aje upesi, yafanyike Esteri aliyoyasema! Mfalme na Hamani wakaja kula karamu, Esteri aliyoifanya. Walipokunywa mvinyo, mfalme akamwuliza Esteri tena: Unataka nini? Utapewa. Unataka nini? Ingawa ni nusu ya ufalme, itafanyika. Esteri akajibu akisema: Ninayoyaomba kwa kuyataka ni haya: kama nimeona upendeleo mbele ya mfalme, kama ni vizuri kwake mfalme kunipa ninayoyaomba na kuyafanya, mfalme na aje tena pamoja na Hamani kula karamu, nitakayowafanyizia kesho; ndipo, nitakapofanya, kama mfalme alivyosema. Hamani akatoka mwake siku hiyo kwa kufurahi na kuchangamka moyoni. Lakini Hamani alipomwona Mordekai langoni kwa mfalme, asiinuke, wala asimwondokee, ndipo, makali yenye moto yalipomjaa Hamani moyoni kwa ajili ya Mordekai, lakini Hamani akajizuia. Alipofika nyumbani mwake, akatuma watu kuwaita wapenzi wake na mkewe Zeresi. Hamani akawasimulia, jinsi utukufu wa mali zake ulivyo mkubwa, tena jinsi wanawe walivyo wengi, nayo macheo yote, mfalme aliyompa akimweka kuwa mkuu kuliko wakuu na watumishi wa mfalme. Kisha Hamani akasema: Naye Esteri, mkewe mfalme, hakualika mwingine, aje na mfalme kula karamu, aliyoifanya, ila mimi peke yangu. Hata kesho mimi nimealikwa naye kuja na mfalme. Lakini haya yote hayanitoshei, nikimwona yule Myuda Mordekai, akikaa siku zote langoni kwa mfalme. Ndipo, mkewe Zeresi na wapenzi wake wote walipomwambia: Na wasimike mti mrefu wa mikono hamsini! Kisha umwambie mfalme kesho, wamtundike Mordekai, upate kwenda pamoja na mfalme karamuni na kufurahi! Shauri hili likampendeza Hamani, akausimika ule mti. Usiku ule mfalme hakupata usingizi, akaagiza, wamletee hicho kitabu cha mambo ya siku yapasayo kukumbukwa. Ikawa, yaliposomwa masikioni pa mfalme, zikaoneka zile habari zilizoandikwa za kwamba: Mordekai ameumbua watumishi wa nyumbani mwa mfalme, Bigitana na Teresi, waliokuwa walinda mlango, waliotafuta njia ya kumwua mfalme Ahaswerosi kwa mikono yao. Mfalme akauliza: Mordekai amepata tunzo gani au ukuu gani kwa tendo hilo? Vijana wa mfalme waliomtumikia wakajibu: Hakuna alichofanyiziwa. Mfalme akauliza tena: Uani yuko nani? Naye Hamani alikuwa ameingia katika ua wa nje wa nyumba ya mfalme, aje kumwambia mfalme, wamtundike Mordekai katika ule mti, aliomsimikia. Vijana wa mfalme walipomwambia: Tazama, ni Hamani anayesimama uani, mfalme akasema: Aje! Hamani alipokuja, mfalme akamwuliza: Mfalme akipendezwa kumheshimu mtu, atafanyiziwa nini huyo mtu? Hamani akawaza moyoni mwake kwamba: Yuko nani, mfalme apendezwaye naye, amheshimu, nisipokuwa mimi? Kwa hiyo Hamani akamwambia mfalme: Kama yuko mtu, mfalme apendezwaye naye, amheshimu, na walete nguo ya kifalme, mfalme aliyoivaa, na farasi, mfalme aliyempanda, aliyevikwa kichwani pake kilemba cha kifalme! Kisha mkuu mmoja wa mfalme mwenye macheo apewe hiyo nguo na huyo farasi, wamvike huyo mtu, mfalme apendezwaye naye, amheshimu, kisha wampandishe huyo farasi uwanjani mwa mji na kupiga mbiu mbele yake kwamba: Hivi ndivyo, mtu anavyofanyiziwa, mfalme akipendezwa naye, amheshimu. Ndipo, mfalme alipomwambia Hamani: Nenda upesi sasa hivi kuichukua hiyo nguo na huyo farasi, kama ulivyosema, umfanyizie vivyo hivyo Myuda Mordekai akaaye langoni kwa mfalme! Lakini usisahau hata neno moja katika hayo, uliyoyasema! Basi, Hamani akaichukua hiyo nguo na huyo farasi, akamvika Mordekai, kisha akampandisha uwanjani mwa mji, akapiga mbiu mbele yake kwamba: Hivi ndivyo, mtu anavyofanyiziwa, mfalme akipendezwa naye, amheshimu. Kisha Mordekai akarudi langoni pake kwa mfalme, lakini Hamani akaikimbilia nyumba yake kwa kusikitika, akawa amejifunika kichwa. Hamani akamsimulia mkewe na wapenzi wake yote yaliyomtukia. Rafiki zake waliokuwa werevu wa kweli na mkewe Zeresi wakamwambia: Kama huyu Mordekai, uliyeanza kumwangukia, ni wa kizazi cha Wayuda, hutamshinda, ila utaendelea kumwangukia. Walipokuwa wangali wakisema naye, wakafika watumishi wa nyumbani wa mfalme, wakamhimiza Hamani, aje upesi kula karamu, Esteri aliyoifanya. Mfalme akaja pamoja na Hamani karamuni kwake Esteri, mkewe mfalme. Walipokunywa mvinyo, mfalme akamwuliza Esteri nayo siku hiyo ya pili: Unaomba nini, Esteri, mkewe mfalme? Utapewa. Unataka nini? Ingawa ni nusu ya ufalme, itafanyika. Ndipo, Esteri, mkewe mfalme, alipomjibu akisema: Kama nimeona upendeleo mbele yako, mfalme, navyo vikiwa vema kwako, mfalme, nipewe roho yangu kwa kuomba kwangu! Tena nipewe wenzangu wa ukoo kwa kutaka kwangu! Kwani tumekwisha kuuzwa mimi na wenzangu wa ukoo, tutoweshwe kwa kuuawa na kwa kuangamizwa. Kama tungaliuzwa tu kuwa watumwa na vijakazi, ningalinyamaza; lakini mpingani huyo hawezi kuvilipa, mfalme akipotelewa na watu hao. Mfalme Ahaswerosi akamwuliza Esteri, mkewe mfalme, na kusema: Ni nani huyu, tena yuko wapi aliyeushupaza moyo wake, upate kuwaza tendo kama hilo? Esteri akamwambia: Mtu wetu mpingani na adui ni huyu Hamani, ni mbaya. Ndipo, Hamani alipostuka mbele ya mfalme na mkewe mfalme. Lakini mfalme akainuka kwa makali hapo penye mvinyo, akaja bustanini kwenye jumba lake. Naye Hamani akasimama kumwomba Esteri, mkewe mfalme, amponye, kwani ameona, ya kuwa liko shauri baya, alilokwisha kukatiwa na mfalme. Mfalme alipotoka kule bustanini kwenye jumba lake na kuingia tena mle nyumbani, waliomkunywa mvinyo, Hamani alikuwa ameanguka penye kitanda, Esteri alipokaa; ndipo, mfalme aliposema: Je, Naye mkewe mfalme anataka kumkorofisha humu nyumbani mwangu? Neno hili lilipotoka kinywani mwa mfalme, ndipo, walipoufunika uso wa Hamani. Harbona, mmoja wao watumishi wa nyumbani waliomtumikia mfalme, akasema: Tazameni, ule mti, Hamani aliomsimikia Mordekai aliyesema mema ya kumponya mfalme, ungaliko kwenye nyumba ya Hamani, ni ule mrefu wa mikono hamsini. Ndipo, mfalme aliposema: Haya! Mtundikeni mumo humo! Wakamtundika Hamani katika ule mti, aliomsimikia Mordekai; kisha makali ya mfalme yakatulia. Siku hiyo mfalme Ahaswerosi akampa Esteri, mkewe mfalme, nyumba ya Hamani, aliyekuwa mpingani wao Wayuda. Mordekai akaja kwa mfalme, kwani Esteri alimsimulia mfalme, udugu wao ulivyo. Ndipo, mfalme alipoondoa kidoleni pete yake yenye muhuri, aliyomvua Hamani, akampa Mordekai. Naye Esteri akamkalisha Mordekai katika nyumba ya Hamani. Esteri akaendelea kusema mbele ya mfalme, akamwangukia miguuni na kulia machozi na kumlalamikia, autangue ule ubaya wa Hamani wa Agagi nayo mashauri yake, aliyowatakia Wayuda. Mfalme alipompungia Esteri kwa bakora yake ya dhahabu, Esteri akainuka, asimame mbele ya mfalme, akasema: Vikiwa vema kwake mfalme, nami nikiwa nimeona upendeleo mbele yake, nalo neno hili likifaa mbele yake mfalme, mimi nikiwa mwema machoni pake, basi, na ziandikwe barua za kuzitangua zile barua zenya lile shauri baya la Hamani, mwana wa Hamedata wa Agagi, alizoziandika za kuwaangamiza Wayuda wote walioko katika majimbo yote ya mfalme. Kwani nitawezaje kuyatazama hayo mabaya yatakayowapata wenzangu wa ukoo? Tena nitawezaje kuutazama mwangamizo wa ukoo wangu? Ndipo, mfalme Ahaswerosi alipomwambia Esteri, mkewe mfalme, na Myuda Mordekai: Tazameni, nyumba ya Hamani nimempa Esteri, naye mwenyewe wamemtundika katika ule mti, kwa kuwa aliunyosha mkono wake, awaue Wayuda. Basi, ninyi andikeni barua kwa Wayuda katika jina la mfalme, kama mnavyoona kuwa vema, kisha zitieni zile barua muhuri kwa hiyo pete ya mfalme! Kwani barua iliyoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme haitanguki. Wakaitwa waandishi wa mfalme wakati huo wa mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani, siku ya ishirini na tatu, yote Mordekai aliyoyaagiza yakaandikwa baruani kwa Wayuda na kwa wenye amri na kwa watawala nchi na kwa wakuu wa majimbo kuanzia nchi ya Uhindi kuifikisha hata nchi ya Nubi, majimbo yote ni 127; yakaandikwa kwa kila jimbo katika maandiko ya kwao na kwa kila kabila katika msemo wa kwao, hata kwa Wayuda katika maandiko ya kwao na katika msemo wa kwao. Naye akaziandika hizo barua katika jina la mfalme Ahaswerosi, akazitia muhuri kwa ile pete ya mfalme yenye muhuri, kisha akawapa wapiga mbio waliopanda farasi, wazipeleke; nao hao farasi waliowapanda walikuwa wa wakuu, walizaliwa katika makundi yaliyochaguliwa. Yaliyoandikwa ni haya: Mfalme amewapa ruhusa Wayuda waliomo katika miji yote, wakusanyike katika kila mji mmoja kujisimamia wenyewe na kujiokoa, wakiwatowesha kwa kuwaua na kwa kuwaangamiza vikosi vyote vya watu wa kila kabila na wa kila jimbo watakaowashambulia, hata watoto na wanawake, kisha waziteke nazo mali zao. Yafanyike siku moja katika majimbo yote ya mfalme Ahaswerosi, ndio siku ya kumi na tatu katika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. Mwandiko wa pili wa hizo barua ukatangazwa katika kila jimbo moja kuwa amri iliyotolewa na mfalme, watu wote pia wakaelezwa vema, Wayuda wapate kuwa tayari siku hiyohiyo kujilipiza kwa adui zao. Wapiga mbio waliopanda farasi wale wepesi wa wakuu wakatoka upesi na kujihimiza kwa ajili ya lile neno la mfalme. Namo mjini mwa Susani, mlimokuwa na jumba la mfalme, ile amri ya mfalme ikatangazwa. Kisha Mordekai akatoka usoni pa mfalme, akawa amevaa vazi la kifalme la nguo ya kifalme nyeusinyeusi na nyeupe, napo kichwani amevaa kilemba kikubwa cha kifalme cha dhahabu, tena amevaa joho la bafta lenye nguo nyekundu za kifalme. Nao mji wa Susani ukajaa vigelegele na mashangilio. Hivyo ndivyo, Wayuda walivyopata machangamko na furaha na macheko na macheo. Katika kila jimbo na katika kila mji mmoja mahali po pote, lile neno la mfalme lilipotangazwa, pakawa na furaha na macheko kwa Wayuda, hata karamu na sikukuu, nao watu wengi wa hizo nchi wakajigeuza kuwa Wayuda, kwa kuguiwa na woga wa kuwaogopa Wayuda. Katika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku ya kumi na tatu ilikuwa ile siku iliyotangazwa kwamba: Lile neno la mfalme, aliloliagiza, lifanyike siku hiyo; ndipo, adui za Wayuda walipongojea kuwashinda, lakini ikageuzwa, Wayuda wakapata wao kuwashinda wachukivu wao. Siku hiyo ilipotimia, Wayuda wakakusanyika katika miji yao katika majimbo yote ya mfalme Ahaswerosi kuwaua kwa mikono yao waliotaka kuwafanyizia mabaya, lakini hakuwako mtu aliyesimama mbele yao, kwani mastusho yaliyaguia makabila yote. Nao wakuu wote wa majimbo nao wenye amri nao watawala nchi nao wenye kazi nyingine za mfalme wakawasaidia Wayuda, kwani woga uliwaguia wa kumwogopa Mordekai. Kwani Mordekai alikuwa mkubwa katika nyumba ya mfalme, nayo sifa yake ikasikilika katika majimbo yote, kwani huyo mtu Mordekai akaendelea kuwa mkubwa zaidi. Wayuda wakawapiga adui zao wote mapigo ya panga, wakawaua, wakawaangamiza, wakawafanyizia wachukivu wao, kama walivyopendezwa. Namo Susani, mlimokuwa na jumba la mfalme, wakaua watu, wakaangamiza watu 500. Wakawaua nao hawa: Parsandata na Dalfoni na Asefata na Porata na Adalia na Aridata na Parmasta na Arisai na Aridai na Yezata; ndio wana kumi wa Hamani, mwana wa Hamedata, aliyekuwa mpingani wao Wayuda; lakini mali zao hawakuziteka kwa mikono yao. Siku hiyo mfalme alipopata hesabu yao waliouawa Susani, mlimokuwa na jumba la mfalme, mfalme akamwambia Esteri, mkewe mfalme: Humu susani, mlimo na jumba la mfalme, Wayuda wameua na kuwaangamiza watu 500 na wana kumi wa Hamani; sijui, waliyoyafanya katika majimbo mengine ya mfalme yaliyosalia. Lakini unayoyaomba utapewa; nayo unayoyataka yatafanyika tena. Esteri akasema: Vikiwa vema kwake mfalme, Wayuda waliomo Susani wapewe ruhusa hata kesho kufanya, kama walivyofanya leo, nao wale wana kumi wa Hamani wawatundike katika ule mti. Mfalme akasema: Na yafanyike hivyo! Kisha hiyo amri ya mfalme ikatolewa mle Susani, nao wale wana kumi wa Hamani wakawatundika. Basi, Wayuda waliokuwamo Susani wakakusanyika hata siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, wakaua mle Susani tena watu 300, lakini mali zao hawakuziteka kwa mikono yao. Nao wale Wayuda wengine waliokuwa katika majimbo wakakusanyika, wajisimamie wenyewe na kujiokoa, wajipatie utulivu kwao adui zao, wakaua wachukivu wao 75000, lakini mali zao hawakuziteka kwa mikono yao. Hayo yalifanyika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari, lakini siku ya kumi na nne wakatulia, wakaifanya kuwa siku ya karamu na ya furaha. Lakini Wayuda waliokuwa Susani wakakusanyika siku ya kumi na tatu na siku ya kumi na nne, wakatulia siku ya kumi na tano, wakaifanya hiyo kuwa siku ya karamu na ya furaha. Kwa sababu hii Wayuda wa mashambani wanaokaa katika miji iliyo wazi huifanya siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kuwa siku ya furaha na ya karamu na sikukuu pia, nao hupeana matunzo mtu na mwenziwe. Mordekai akayaandika maneno hayo yote akituma barua kwa Wayuda wote waliokaa katika majimbo yote ya mfalme Ahaswerosi, kwao waliokuwa karibu nako kwao waliokuwa mbali, Akawaagiza kuishika desturi hii ya kuzifanya siku ya kumi na nne na ya kumi na tano ya mwezi wa Adari, mwaka kwa mwaka, kuwa sikukuu, kwa kuwa ndipo, Wayuda walipopata kutulia kwa adui zao; kwa hiyo ni mwezi, majonzi yao yalipogeuzwa kuwa furaha, nayo masikitiko yao kuwa siku nzuri. Kwa sababu hii wazifanye siku hizo kuwa za karamu na za furaha na za kupeana matunzo mtu na mwenziwe, nao wakiwa sharti wapelekewe vipaji. Ndipo, Wayuda walipoitikia kuendelea kuyafanya, waliyoyaanza hapo; ndiyo, Mordekai aliyowaandikia. Kwani ndipo, Hamani, mwana wa Hamedata wa Agagi, aliyekuwa mpingani wa Wayuda wote, alipowazia kuwaangamiza Wayuda kwa hivyo, alivyokuwa amewapigia Puri, ndiyo kura, awatoweshe kwa kuwaangamiza. Lakini mfalme alipopashwa habari hizo alikuwa ameagiza kwa barua kwamba: Wazo hilo baya, alilowawazia kuwafanyizia Wayuda, sharti limrudie kichwani pake, wamtundike yeye na wanawe mtini. Kwa sababu hii sikukuu hizi wakaziita Purimu wakilifuata lile neno la Puri (kura). Kwa ajili ya maneno yote ya barua hiyo na kwa ajili yao, waliyoyaona wenyewe, na kwa ajili yao, wengine waliyowasimulia, kwa kuyaitikia yale Wayuda wakaagiza, kwao nako kwao wa uzao wao nako kwao wote watakaojiunga nao iwe desturi isiyotanguka ya kuzishika hizo siku mbili hapo, siku zao zilizowekwa zitakapotimia kila mwaka utakaokuwa, kama yalivyoandikwa. Kwa sababu hii sikukuu hizi zikumbukwe, zishikwe kwa kila kizazi na kwa kila mlango katika kila jimbo na katika kila mji; hizo sikukuu za Purimu zisikome kabisa kwao Wayuda, wala ukumbusho wao usitoweke kwao wa uzao wao. Kisha Esteri, mkewe mfalme, mwana wa Abihaili, na Myuda Mordekai wakaandika barua ya pili na kuwashurutisha watu kwelikweli na kuwaagiza kuzishika hizo sikukuu za Purimu. Akatuma hiyo barua kwa Wayuda wote katika yale majimbo 127 ya ufalme wa Ahaswerosi na kuwaambia maneno ya utengemano wa kweli. Akaagiza kuzishika hizo sikukuu za Purimu siku zilezile, walizowaagiza Myuda Mordekai na Esteri, mkewe mfalme, kama walivyojiagizia wenyewe nao wa uzao wao mambo ya mifungo na ya maombolezo yao. Amri ya Esteri iliyoyaagiza mambo ya hizo sikukuu za Purimu ikaandikwa katika kitabu. Mfalme Ahaswerosi akatoza kodi katika hiyo nchi, hata katika visiwa vya baharini. Matendo yote ya uwezo wake na ya nguvu zake na habari zote za macheo makuu, mfalme aliyompa Mordekai, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wao Wamedi na Wapersia? Kwani Myuda Mordekai alikuwa wa pili kwake mfalme Ahaswerosi na mkuu kwa Wayuda, akapendwa na ndugu zake waliokuwa wengi, kwa kuwa aliwatakia mema walio ukoo wake, akasema nao wote walio wa kizazi chake maneno ya utengemano. Kulikuwa na mtu katika nchi ya usi, jina lake Iyobu. Mtu huyu alikuwa mnyofu wa kweli mwenye kumcha Mungu, nayo mabaya alikuwa ameyaepuka. Kwake walizaliwa wana saba wa kiume na watatu wa kike. Makundi yake yalikuwa mbuzi na kondoo pamoja 7000 na ngamia 3000 na majozi ya ng'ombe 500 na punda majike 500, hata watumwa wake wakawa wengi sana. Kwa hiyo yule mtu alikuwa mkuu kuliko watu wote waliokaa upande wa maawioni kwa jua. Wanawe wa kiume walifanya nyumbani mwake kila mmoja sikukuu yake; ndipo, walipowaalika maumbu zao watatu kula na kunywa pamoja nao. Ikawa, kila walipozila hizo sikukuu zao, Iyobu hutuma kwao, akawatakasa kesho yake asubuhi akiwatolea ng'ombe za tambiko, wao wote kila mtu yake, kwani Iyobu alisema: Labda wanangu wamekosa wakiacha kumcha Mungu mioyoni mwao. Hivyo ndivyo, Iyobu alivyovifanya siku zote. Ikawa siku moja, wana wa Mungu walipokuja kumtokea Bwana, Satani naye akaja katikati yao. Bwana akamwuliza Satani: Umetoka wapi? Satani akamjibu Bwana akisema: Natoka katika kutembea katika nchi na kujiendea huko na huko. Bwana akamwuliza Satani: Umemwangalia mtumishi wangu Iyobu? Kwani katika nchi hakuna mtu kama yeye, ni mnyofu wa kweli mwenye kumcha Mungu, nayo mabaya ameyaepuka. Satani akamjibu Bwana akisema: Je? Iyobu anamcha Mungu bure? Wewe humwangalii mwenyewe na nyumba yake nayo yote yaliyo yake po pote? Ukazibariki kazi za mikono yake, nayo makundi yake yameieneza nchi. Haya! Ukunjue mkono wako, uyapige yote yaliyo yake! Ndipo, atakapokutukana usoni pako. Bwana akamwambia Satani: Tazama, yote yaliyo yake nakupa! Ila yeye mwenyewe tu usimguse kwa mkono wako! Ndipo, Satani alipotoka usoni pake Bwana. Ikawa siku moja, wanawe wa kiume na wa kike walipokula sikukuu na kunywa nvinyo nyumbani mwa ndugu yao aliyezaliwa wa kwanza, mjumbe akaja kwake Iyobu, akamwambia: Ng'ombe walipokuwa wanalima, nao punda walipolisha kando yao, mara watu wa Saba wakatushambulia, wakawachukua, nao vijana wakawapiga kwa ukali wa panga zao, mimi nikapona peke yangu tu, nikupashe habari. Huyu angali akisema, akaja mwingine, akasema: Moto wa Mungu umeanguka toka mbinguni, ukawaka kwenye mbuzi na kondoo, ukawala pamoja na vijana, mimi nikapona peke yangu tu, nikupashe habari. Huyu angali akisema, akaja mwingine, akasema: Wakasidi wamekuja vikosi vitatu, wakatushambulia, wakawakamata ngamia, wakawachukua, nao vijana wakawapiga kwa ukali wa panga zao, mimi nikapona peke yangu tu, nikupashe habari. Huyu angali akisema, akaja mwingine, akasema: Wanao wa kiume na wa kike walipokula sikukuu na kunywa nvinyo nyumbani mwa ndugu yao aliyezaliwa wa kwanza, mara upepo mkubwa uliotoka upande wa nyika ukazipiga pembe zote nne za ile nyumba, ikawaangukia wale vijana, wakafa; mimi nikapona peke yangu tu, nikupashe habari. Ndipo, Iyobu alipoinuka, akazirarua nguo zake, akajinyoa kichwa chake, akajitupa chini kumwangukia Mungu, akasema: Nilipotoka tumboni mwa mama nilikuwa mwenye uchi, tena nitakapotoka huku nitakuwa mwenye uchi vilevile. Bwana ndiye aliyenipa, Bwana ndiye aliyeyachukua tena, Jina la Bwana na litukuzwe! Katika mambo hayo yote Iyobu hakukosa, wala hakumwazia Mungu kuwa mwenye mambo yasiyopasa. Ikawa siku nyingine, wana wa Mungu walipokuja kumtokea Bwana, Satani naye akaja katikati yao kumtokea Bwana. Bwana akamwuliza Satani: Umetoka wapi? Satani akamjibu Bwana akisema: Natoka katika kutembea katika nchi na kujiendea huko na huko. Bwana akamwuliza Satani: Umemwangalia mtumishi wangu Iyobu? Kwani katika nchi hakuna mtu kama yeye, ni mnyofu wa kweli mwenye kumcha Mungu, nayo mabaya ameyaepuka, hata sasa angali anajikaza, asinikosee, ingawa umenichochea kumwangamiza bure. Satani akamjibu Bwana akisema: Ngozi hulipwa ngozi. Mtu huyatoa yote yaliyo yake, aiponye roho yake. Haya! Ukunjue mkono wako, uipige mifupa na nyama za mwili wake! Ndipo, atakapokutukana usoni pako. Bwana akamwambia Satani: Haya! Namtia mkononi mwako, lakini iangalie roho yake! Ndipo, Satani alipotoka usoni pake Bwana, akampiga Iyobu na kumwuguza majipu mabaya kutoka kwenye wayo hata utosini. Naye akatwaa kigae cha kujikunia, akajikalia majivuni. Ndipo, mkewe alipomwambia: Na sasa ungali unajikaza bado, usimkosee Mungu? Mtukane Mungu! Kisha ufe! Akamwambia: Unasema, kama wanawake wapumbavu wanavyosema; mema tuliyapokea mikononi mwa Mungu, sasa hiki kibaya tusikipokee? Katika mambo hayo yote Iyobu hakukosa kwa midomo yake. Rafiki zake Iyobu watatu walipoyasikia hayo mabaya yote yaliyompata, ndipo, walipoondoka kila mtu mahali pake, Elifazi wa Temani na Bildadi wa Sua na Sofari wa Nama, wakapatana kwenda pamoja kumpongeza na kumtuliza moyo. Wakayainua macho yao walipokuwa wako mbali bado, lakini hawakumtambua, wakapaza sauti zao, wakalia, wakazirarua nguo zao, kila mtu zake, wakajimwagia mavumbi kichwani na kujielekeza mbinguni. Wakakaa pamoja naye chini siku saba mchana kutwa na usiku kucha, hakuna aliyeweza kumwambia neno, kwani waliyaona maumivu yake kuwa makubwa mno. Kisha Iyobu akakifumbua kinywa chake, akaiapiza siku yake; yeye Iyobu akaanza kusema kwamba: Siku niliyozaliwa ingalifaa, kama ingaliangamia, pamoja na usiku ule, waliposema: Mimba hii ni mtoto wa kiume. Siku hiyo ingalifaa, kama ingalikuwa yenye giza, kama Mungu wa huko juu asingaliitafuta, kama mchana nao usingaliiangaza. Giza lenye kivuli kiuacho na liitake kuwa lake, mawingu yenye weusi na yaikalie na kuifunika, yageuzayo mchana kuwa giza na yaipatie vituko. Kama giza tupu lingaliupokonya, usiku ule nao ungalifaa, kama usingalihesabiwa katika siku za mwaka huo, wala kama usingaliingia katika hesabu ya miezi! Ningeuona kuwa mwema, kama usingalizaa kitu, wala kama usingalisikia sauti ya shangwe. Wajuao kuziloga siku sharti wauapize, ndio wao waliojipa mioyo kumchochea naye nondo wa baharini. Nyota zake za mapambazuko na ziguiwe na giza, usione mwanga ukiungojea, wala vishale vya mapambazuko usivione, kwa kuwa haukufunga mlango wa tumbo la mama yangu na kuyaficha masumbuko, macho yangu yasiyaone! Mbona sikuweza kufa nilipotoka tumboni mwa mama? Mbona sikuzimia nilipotoka tumboni mwake? Mbona nilipokelewa na kuwekwa magotini? Mbona nikapata maziwa ya kuyanyonya? Kama sivyo, ningelala sasa na kutulia, ningelala usingizi na kujipatia mapumziko; ningekuwa pamoja na wafalme na wenye hukumu wa nchi waliojijengea machuguu makubwa ya kuzikiwa humo; au ningekuwa pamoja na wakuu waliokuwa wenye dhahabu, waliozijaza nyumba zao na kulimbika fedha; au ningalikwisha kuchimbiwa tu kama mimba iliyoharibika, nisipate kuwapo kama wachanga wasiouona mwanga. Huko ndiko, wanakokomea kuchafuka wasiomcha Mungu; ndiko, wanakopumzikia waliojichokesha kwa kuzitumia nguvu zao. Huko wafungwa wote pamoja hutengemana, hawasikii tena sauti ya msimamizi. Huko wadogo na wakubwa ni wamoja, nao watumwa wamekwisha kombolewa, wasiwe mali za mabwana zao. Sababu gani anampa msumbufu kuona mwanga? Sababu gani anampa kuwapo mwenye uchungu rohoni? Ndio wanaokingojea kifo, lakini hawakipati; kuliko vilimbiko vilivyofichwa hutaka kukizua. Hao wangefurahi na kushangilia, wangechangamka kweli, kama wangeona kaburi. Hao ni watu waliofichwa maana ya njia zao, wao ndio, Mungu aliowazibia mizungu yote pia. Sharti kwanza nipige kite, ninapotaka kula, navyo vilio vyangu humwagika kama maji. Kwani ninapostukia kistusho, hichohicho hunipata, nacho nilichokiogopa hunijia. Sipati kutengemana wala kutulia wala kupumzika, kwani mahangaiko hunijia. Elifazi wa Temani akamjibu akisema: Mtu akijaribu kukuambia neno, litakukasirisha? Lakini yuko nani awezaye kujizuia, asiseme? Tazama, uliowaonya ni wengi, ukashupaza mikono iliyokuwa imelegea. Maneno yako yakawainua waliojikwaa, nayo magoti yaliyokuwa yamechoka ukayatia nguvu. Lakini sasa mambo yakikufikia wewe, unazimia; yakikugusa wewe nawe, unastuka. Hivyo, unavyomcha Mungu, sivyo unavyoviegemea? tena hivyo, njia zako zinavyomwelekea Mungu, sivyo unavyovingojea? Kumbuka, kama yuko aliyeangamia akiwa hakukosa? tena wako wapi wanyokao waliotoweshwa? Nilivyoviona ni hivi: wenye kulima mapotovu nao wenye kupanda masumbuko, huyavuna yayo hayo. Mungu akiwapuzia, huangamia; akiwafokea kwa ukali wake humalizika. Sauti zake simba huwa zenye ukali, akinguruma; lakini meno yao wana wa simba yakivunjika, nao hukosa nyama za kula; ndivyo, naye simba anavyoangamia, nao watoto wa simba mke hutawanyika. Liko neno lililonijia kama mwizi, sikio langu likalipokea, liliponong'onezwa. Usiku uliponitia mawazo mengine kwa kuniotesha, ilikuwa hapo, watu wanapoangukiwa na usingizi mzito; ndipo, kistusho kiliponipata na kunitetemesha, mifupa yangu yote ikafa ganzi, upepo ukapita usoni pangu, mara nywele za mwili wangu zikajisimamisha, kwani pakasimama mfano machoni pangu, nami sikuweza kuutambua vema, jinsi ulivyokuwa; lakini kwa kuwa kimya nikasikia sauti ya kwamba: Je? yuko mtu aongokaye kuliko Mungu? Je? yuko wa kiume atakataye kuliko yeye aliyemwumba? Tazama! Watumishi wake hawezi kuwategemea, nao malaika zake huwaona, wakikosa. Sembuse wao wakaao katika nyumba za udongo, ambazo waliziwekea misingi uvumbini? Wao ndio wanaopondwa, kama ni nondo tu. Toka asubuhi mpaka jioni husetwasetwa; nao wakiangamia kale na kale, hakuna aviwekaye moyoni. Kamba za mahema yao hakatwa, wakingali wamo; kwa kukosa werevu wa kweli hujifia tu. Haya! Ita, kama yuko mtu anayekuitikia! Kwao walio watakatifu utamtokea nani? Kwani majonzi humwua mjinga, nao wivu humwua mpuzi. Mimi niliona mjinga, akishusha mizizi, lakini mara sikuwa na budi kuliapiza hilo kao lake. Watoto wake hawakupata wokovu, uliwakalia mbali, Walipowaponda langoni, hakuwako mponya. Mavuno yake yakaliwa na mwingine aliyekuwa na njaa, akayachukua na kuyatoa penye vitalu, ingawa ni vyenye miiba, nao wenye kiu huzitwetea mali zao. Kwani upotovu hautoki uvumbini, wala usumbufu hauchipuki hapa nchini, ila mtu huzaliwa, apate kusumbuka, awe kama cheche za moto zinazoruka juu. Lakini aliye Mungu mimi ningemtafuta, naye Mungu ningemwambia shauri langu. Hufanya mambo makuu yasiyochunguzika, vioja vyake havihesabiki: hutoa mvua kuinyesha nchi, ayapatie mashamba maji ya juu. Walio wanyenyekevu huwakweza, huwapandisha kuufikia wokovu wao wasikitikao. Huyatangua mawazo yao walio werevu, mikono yao isiweze kufanya kifaacho. Nao wenye ubingwa huwakamata kwa werevu wao, mashauri yao wapotovu yaangamie upesi. Nao mchana wao huguiwa na giza, wapapasepapase mnamo saa sita, kama ni usiku. Ndivyo, anavyowaokoa wamaskini, ukali wa upanga usiwaue, wala mikono ya wenye nguvu isiwashinde. Hivyo ndivyo, kingojeo kinavyomtokea naye mnyonge, lakini uovu hufumbwa kinywa chake. *Tazama! Mwenye shangwe ni mtu, Mungu anayemchapa! Kwa hiyo usikatae kuonywa na Mwenyezi! Kweli yeye huumiza, lakini tena huuguza; atakapotia kidonda, mikono yake hukiponya. Atakuokoa katika masongano sita, yawe hata saba, kisioneke kibaya kitakachokugusa. Penye njaa atakukomboa namo kufani, hata vitani atakukomboa mikononi mwao wenye panga. Penye mapigo ya ndimi za watu utafichika, usiogope hapo napo, mwangamizo utakapokuja; utaucheka mwangamizo, hata njaa, nao nyama wakali wa nchi hutawaogopa. Kwani nayo mawe ya mashambani utapatana nayo, nao nyama wa porini watatengemana huko, uliko. Ndipo, utakapolijua hema lako kuwa lenye utengemano, napo utakapolitazama kao lako, hutaona kitakachokoseka. Tena utayaona mazao yako kuwa mengi, navyo vizazi vya kwako vitakuwa vingi kama majani ya nchi. Nguvu zako zitakuwa hazikupunguka, utakapoingia kaburini, kama viganda vinavyoingizwa, mavuno yanapotimia.* Tazama! Haya tumeyachunguza kuwa hivyo kweli; yasikie, nawe upate kuyajua moyoni mwako! Iyobu akajibu akisema: Kama yangepimwa machafuko yangu, wakiyatia nayo mateso yangu katika mizani, haya yangetokea kuwa mazito zaidi kuliko mchanga wa baharini; kwa hiyo maneno yangu ni ya kupotelewa tu. Kwani mishale ya Mwenyezi imenipiga, nayo sumu yao yenye moto roho yangu ikainywa, vitisho vya Mungu vikajipanga kuninasa mimi. Je? Punda wa porini hulia mbugani penye majani? Au yuko ng'ombe apigaye kelele penye chakula chake? Au visivyoungwa huliwa pasipo chumvi? Au yako yapendezayo, ukila ute wa yai? Roho yangu inakataa kuvigusa tu, kwani hufanana na vyakula vyangu vichukizavyo. Laiti yangetimia niyatakayo, Mungu akinipa niyangojeayo! Kama Mungu yangempendeza, na aniponde, na aukunjue mkono wake kuikata roho yangu! Litakalonituliza moyo litakuwako nayo siku hiyo, ijapo niumizwe pasipo kuhurumiwa, lilo hilo litanichezesha, ndio hilo la kwamba: Sikuyakana maneno yake Mtakatifu! Nguvu zangu ni za nini, nitulie na kungoja? Mwisho wangu utakuwaje, nipate kuvumilia? Je? Kama nguvu za mawe zilivyo, ndivyo, nguvu zangu zilivyo nazo? Au mwili wangu, nilio nao, ni wa shaba? Je? Haya hayakunipata kwa kukosa msaada wo wote? Je? Uponya haukutoweshwa huku, niliko? Mwenye kuzimia hupaswa na rafiki wamwendeao kwa upole, ijapo amekwisha kuacha kumcha Mwenyezi. Ndugu zangu wameniacha na kudanganya kama kijito, kama mikondo ya vijito vikaukavyo upesi; maana hivi huwa vyeusi kwa maji ya barafu, theluji ziyeyukazo zilimoingia kujifichia humo. Lakini siku, vinapowakiwa na jua, hupwa, hutoweka mahali pao, kiangazi kikitimia. Misafara huziacha njia zao kuvipandia jangwani, lakini wasipokuta kijito chenye maji, huangamia. Misafara ile ya Tema huvitazamia, vikosi vya Saba huvingojea katika safari zao. Lakini huona kuwa bure kuvikimbilia, kwani wanapofika mahali pao wamedanganyika. Nanyi sasa mmeniwia vivyo hivyo: mlipoyaona haya mastusho mkashikwa na woga. Je? Nimewaambia: Nipeni? Kwa mali zenu ninyi nikomboeni? Au: Niponyeni mkononi mwake anisongaye, namo mikononi mwao wakorofi nikomboeni? Nifunzeni, nipate kunyamaza! Nitambulisheni, nilipopotea! Maneno yanyokayo hushinda kweli, lakini maneno yenu ya kunisuta yana maana gani? Je? Mwawaza mioyoni mwenu kuonya maneno tu? Maneno ya mtu azimiaye ni ya upepo tu. Hata mwana aliyefiwa na wazazi mwaweza kumpigia kura, mkamwuza naye aliye mwenzenu. Lakini sasa ninawaomba, mnielekee mimi; sitaweza kuwaongopea usoni penu. Rudini, msifanye upotovu! Rudini, mwone, wongofu wangu ungaliko. Je? Ulimi wangu umesema yaliyo mapotovu? Au kinywa changu hakiyatambui yaponzayo? Je? Mtu hashurutishwi kufanya kazi ya vita huku nchini? Siku zake si sawa kama siku zake mkibarua? Huwa kama mtumwa atweteaye kivuli, au kama mkibarua aungojeaye mshahara wake. Vivyo hivyo nami nimepewa miezi ya kuteseka, iwe fungu langu, nikagawiwa masumbuko usiku kwa usiku. Ninapolala nasema: Nitainuka lini? kwani saa za usiku huwa ndefu sana, nikazidi kujigeuzageuza kitandani, mpaka kuche. Nyama za mwili wangu zimevikwa funyo na maganda yenye vumbi, ngozi yangu inapopona kidonda, papo hapo hutumbuka jipu tena. Siku zangu hupita upesi sana kuliko chombo cha kufumia, sinacho kingojeo cho chote, ila zimalizike tu. Kumbuka, ya kuwa siku zangu za kuwapo ni pumzi tu, jicho langu halitarudi huku, lipate kuona mema. Jicho lake anionaye sasa halitanitazama tena, macho yako yatakaponielekea, nitakuwa sipo. Kama wingu linavyopoteleapotelea, mpaka litoweke, vivyo hivyo naye ashukaye kuzimuni hatokei tena; hawezi kurudi tena, aingie nyumbani mwake, wala mahali pake, alipokuwa, hapamtambui tena. Kwa hiyo mimi sitakizuia kinywa changu, niseme kwa kusongeka rohoni mwangu, nilie kwa uchungu wa moyo wangu. Je? Mimi ni kama bahari au kama nyangumi, ukiniwekea watu wa kuniangalia? Nikisema: Kilalo changu ndicho kitakachonituliza moyo, kitanda changu kitanipunguzia vilio vyangu, ndipo, unaponitisha kwa kuniotesha ndoto, kwa kunionyesha maono unanistusha. Kwa hiyo roho yangu inapenda kunyongwa tu, kuliko kuwa gofu la mtu, kama nilivyo, inapenda kufa kweli. Nimekata tamaa kwa kukataa kuwapo kale na kale; kwa sababu siku zangu ni za bure, uniache tu! Mtu ndio nini, ukimkuza, ukimwelekezea moyo wako, umwangalie? Ukimkagua kila kunapokucha? Ukimjaribu punde kwa punde? Mbona hutakoma kunitazama? Hutaniacha peke yangu, niyameze mate yangu? Kama nimekosa, nimekufanyia nini, wewe mlinda watu? Mbona umeniweka kuwa shabaha yako ya kuipiga, mpaka nikijiona mwenyewe kuwa mzigo? Mbona huniondolei maovu yangu, ukazitowesha nazo manza, nilizozikora? Kwani sasa ninakwenda zangu kulala uvumbini; utakaponitafuta mapema utaniona, sipo. Kama hayo utayasema hata lini? Maneno ya kinywa chako yatavuma hata lini yakiwa kama upepo wa kimbunga? Je? Yako maamuzi, Mungu anayoyapotoa? Au yako yanyokayo, Mwenyezi anayoyapotoa? Kwa kuwa wanao walimkosea, amewatwika maovu yao. Lakini wewe ukimtafuta Mungu mapema na kumlalamikia Mwenyezi, ukiwa umetakata, ukanyoka, kweli ataamka sasa hivi, aje kwako, alitengemanishe kao lako, wongofu wako ukae humo; ndipo, mali zako za kwanza zitakapokuwa chache, maana zako za mwisho zitazidi kuwa nyingi mno. Walio wa kizazi cha kale waulize wao, kajishikize kwa mambo ya baba zao, waliyoyachunguza! Kwani sisi tu wa jana tu, hatujui neno, kwani siku zetu ni kama kivuli kipitacho katika nchi. Hao sio watakaoweza kukufunza wakikuelezea mambo, wakitoa mioyoni mwao watakayokuambia? Je? Pasipokuwa penye unyevu huotesha matete? Pasipokuwa penye maji huchipuza mafunjo? Siku za kuyakata zitakapotimia, yako majani ya kwanza tu; majani mengine yakiwa mabichi bado, yale yamekwisha kukauka. Hivyo ndivyo, zilivyo njia zao wale waliomsahau Mungu, ndivyo, kinavyoangamia kingojeo cha mpotovu. Kwani egemeo lake litavunjika, nalo kimbilio lake ni tando la buibui. Akijiegemeza penye nyumba yake, haisimani, akiishika kwa nguvu, haikai. Naye akiwa mwenye utomvu mwingi, ijapo jua liwe kali, nayo machipukizi yake yakilieneza shamba lake, mizizi yake ikizinga nazo chungu za mawe, ikijiingiza kwa nguvu zao namo maweni penye nyumba: lakini wakimng'oa mahali pake, alipokuwa, ndipo, hapo pake patakapomkana kwamba: Sijakuona. Tazama! Hii ndiyo furaha, njia yake inayompatia, kisha wataota wengine hapo uvumbini, alipokuwa. Utaona, Mungu hamtupi mtu asiyekosa, lakini wafanyao mabaya hawashiki mikono. Kweli kinywa chako atakijaza vicheko, midomo yako nayo na ishangilie. Lakini watakaoiva nyuso kwa soni ndio wachukivu wako, nayo mahema yao wasiomcha Mungu yatakuwa hayako. Iyobu akajibu akisema: Najua, hii ni kweli; ndivyo, vilivyo kweli: Sisi watu hakuna aliye mwongofu mbele yake Mungu. Kama anataka kuulizana na mtu, akimwuliza maneno elfu, moja tu hawezi kumjibu. Moyo wake ni wenye werevu wa kweli, naye ni mwenye nguvu nyingi, yuko nani aliyejishupaza kushindana naye, akapona? Aondoa milima na kuiweka pengine, isivijue, makali yake yakiwaka, anaifudikiza. Anaitetemesha nchi, itoweke mahali pake, nayo mashikizo yake yatikisike sana. Akiliagiza jua, halichi, nazo nyota anazifunga na kuzitia muhuri. Yeye peke yake ndiye anayezitanda mbingu, anatembea na kuyakanyaga mawimbi ya bahari. Yeye ndiye aliyezitengeneza nyota, kama za Gari nazo za Choma, nikuchome, hata za Kilimia, nazo zile za mifanofano iliyoko upande wa kusini. Hufanya mambo makuu yasiyochunguzika, navyo vioja vyake havihesabiki. Tazama! Akinikaribia na kujiendea tena, simwoni, wala simtambui, akipita. Tazama! Yuko nani awezaye kumrudisha nyuma, akipokonya? Yuko nani awezaye kumwuliza: Unafanya nini? Kwa kuwa Mungu haachi kukasirika, nao wanaosaidiana na nondo wa baharini hawana budi kumwangukia. Sembuse mimi nitawezaje kumjibu lo lote? Mbele yake nitawezaje kuchagua maneno yafaayo? Ingawa niwe sikukosa, nisingemjibu, ila kwa kuwa ni mwamuzi wangu, ningemlalamikia tu. Kama ningemwita, akaniitikia, nisingemtegemea kwamba: Ataisikia sauti yangu. Kwa kunijia na nguvu za chamchela yeye ameniponda, akanitia vidonda vingi zaidi pasipo kosa langu lo lote. Tena haniachi kabisa, nipate kutoa pumzi tu, kwani machungu ndiyo, anayonishibisha. Kama ninatazamia nguvu, nimekwisha kumwona, anavyoshupaa; kama ninatazamia kupiga shauri, yuko nani atakayenishuhudia? Ingawa niwe mwenye wongofu, kinywa changu kingeniponza; kingenitokeza kuwa mpotovu, ingawa niwe sikukosa. Mimi ni mtu asiyekosa. Kuzimia kwa roho yangu nakuwazia kuwa si kitu, huku kuwapo kwangu kunanichukiza. Yote ni mamoja; kwa hiyo nasema: Wasiokosa nao wasiomcha yeye huwaangamiza wote. Akiwapatia watu mapigo ya kuwaua kwa mara moja, huwasimanga nao wasiokora manza, wakiyeyuka. Nchi hii imetiwa mikononi mwao wasiomcha Mungu, naye huzifunika nyuso zao waamuzi wake; kama siye yeye mwenyewe mwingine yuko wapi? Nazo siku zangu hupita upesi sana kuliko mpiga mbio, ijapo, hazikuona mema hujikimbilia. Zimepita upesi kama mitumbwi ya matete, zinafanana na tai, akiangukia chakula. Ikiwa, niseme: Na nivisahau hivi vinavyoniliza, na niache kununa usoni, nichangamke, maumivu yangu yote hunistusha, kwani najua: hutanitokeza kabisa kuwa mtu asiyekosa. Basi, kwa kuwa mimi nitatokezwa kuwa mtu asiyemcha Mungu, nijichokeshe bure tena, nipate nini? Ingawa ningejitawaza kwa maji ya theluji, au ningeinawa mikono yangu kwa sabuni, hapo napo ungenichovya shimoni mwenye machafu, nguo zangu mwenyewe zinitapishe. Kwani Mungu si mtu kama mimi, nimjibu, tukaja kukutana shaurini kuamuliwa. Kwetu sisi, yeye na mimi, hakuna awezaye kutuamua, akitushika sote wawili kwa mkono wake. Na aiondoe fimbo yake, isinipige, vitisho vyake visinistushe! Ndipo, nitakaposema pasipo kumwogopa, kwani hivyo sivyo, mimi nionavyo moyoni mwangu. Roho yangu inachukizwa na kuwapo kwangu, kwa hiyo sitajikataza kupiga kite, na niseme kwa uchungu wa roho yangu. Nitamwambia Mungu: Usiniwazie kuwa mwovu! Ila nijulishe sababu za kunigombeza! Je? Kwako ni vema, ukimkorofisha mtu? Kiumbe, mikono yako ilichokisumbukia, ukatitupa, uyaangaze mashauri yao wasiokucha? Je? Wewe nawe unayo macho ya kimwili? Kama mtu anavyoona, ndivyo, unavyoona nawe? Kama siku za mtu zilivyo, ndivyo, zilivyo nazo siku zako? Au miaka yako inafanana nazo siku zake mtu mume? Kwani unaninyatia, uone manza, nilizozikora, ukayatafuta makosa yangu mimi. Tena unanijua kuwa mtu asiyeacha kukucha, ya kuwa hakuna atakayeniponya mkononi mwako. Mikono yako ndiyo iliyoniumba na kunitengeneza, ikanipatia yote, niliyo nayo, nawe unaniangamiza! Kumbuka, ya kuwa ulinifinyanga kama udongo! Tena unataka kunirudisha uvumbini? Kama maziwa mabichi ulinimwaga ukanigandisha kuwa kama maziwa mabivu. Kisha ukanivika ngozi na nyama, kazi ya kuiunga mifupa na mishipa yangu, ilipokuwa imekwisha. Ukanipatia uzima na upendeleo, ukaikagua roho yangu na kuiangalia. Tena ukaficha moyoni mwako mawazo kama hayo, najua, ya kuwa unayo kweli yale ya kutaka, uniangalie, kama ninakosa, usinikomboe katika manza, nitakazozikora. Kama nafanya maovu, nitaangamia; lakini hata nisipokosa, sitaweza kukiinua kichwa changu, kwani nashiba kwa kuona soni nikiutazama unyonge wangu. Kama kichwa changu kingeinuka, ungenikimbiza kama simba, ukanirudia na kunionyesha mastaajabu yako; ungetoa mara kwa mara mashahidi wa kunisuta, upate kuyazidisha makali ya kunitolea, wawe vikosi vizima vyao wanaopokeana kunitesa. Kwa sababu gani ulinitoa tumboni mwa mama? Macho ya watu yalipokuwa hayajaniona bado, ningalizimia hapo, ningalikuwa kama mtu asiyepata kuwapo, ningalipelekwa kaburini hapo, nilipotoka tumboni mwa mama. Siku zangu zilizosalia si chache tu? Kwa hiyo na akome, na aniache, nipate kuchangamka kidogo, nikiwa sijaenda bado hapo, ambapo sitaweza kutoka, nirudi huku, nikikaa katika ile nchi yenye giza penye kivuli kiuacho; ni nchi yenye giza jeusi kama usiku wa manane, ni nchi ikaayo kivuli kiuacho, tena ni nchi ikosayo matengenezo yo yote, nayo ikiangazika huwa vilevile kama usiku wa manane. Sofari na Nama akajibu akisema: Maneno mengi kama hayo yasijibiwe? Au mtu ajuaye kusema hivyo atakuwa mwongofu? Watu wengine wayanyamazie tu mapuzi yako, asioneke mtu atakayekutweza, wewe ukimfyoza? Wewe tu useme: Maelezo yangu ni ya kweli, nami nimetakata machoni pako? Laiti Mungu akutolee maneno kwa kusema na kuifumbua midomo yake, akushinde! Akakufunulia navyo vilindi vya ujuzi wa kweli vilivyofichwa, kwani mizungu iliyomo hufaa mara mbili; ndipo, utakapojua, ya kuwa Mungu amekuondolea manza, ulizozikora. Je? Waweza kuuvumbua mwanzo wake Mungu usiochunguzika? Au waweza kuyapambazua yake Mwenyezi yatakayokuwa ya mwisho? Yakiwa juu mbinguni, utafanyaje? Yakiwa chini ndani kupita kuzimuni, utajuaje? Ukitaka kuupima urefu wake, unaupita wa nchi, nao upana wake unaupita wa bahari. Yeye akitokea na kupita, afunge watu, yuko nani awezaye kumrudisha nyuma, aliyempeleka shaurini? Kwani yeye anawajua wasiofaa kitu, huwaona waovu, ijapo asiwaangalie. Hapo naye mwenye kichwa kikosacho akili sharti aerevuke, kwani mtu huwa kama mwana wa punda wa nyikani siku akizaliwa. Kama wewe ungeulinganya vema moyo wako, na kumkunjulia mikono yako, kama ungeuondoa uovu uliomo mkononi mwako, ujiendee mbali, kama ungeukataza upotovu kukaa hemani mwako, basi, ungeweza kuuinua uso wako pasipo uchafu wo wote; kwa kuwa umeshikizwa vema, usiogope cho chote! Ndipo, wewe utakapoyasahau nayo masumbuko, yatakuwa kama maji yaliyokupwa hapo, utakapoyakumbuka. Ndipo, utakapotokewa na siku ziangazazo kuliko jua la mchana, napo palipokuwa na giza patakuwa kama mapambazuko. Kwa kuwa na kingojeo utapata cha kukijetea, utakapochungulia nyumbani mwako utalala na kutulia. Tena hatakuwako atakayekustusha hapo, utakapolala, nao wengi watajipendekeza usoni kwako. Lakini macho yao wasiomcha Mungu yataingiwa na kiwi, mahali pa kupakimbilia patawapotelea, kingojeo chao kitakuwa hiki tu: kutoa roho. Iyobu akajibu akisema: Kweli, ninyi tu ndio walio watu, werevu wa kweli utakufa nao, mtakapokufa ninyi. Mimi nami ninazo akili kama ninyi, sikupungukiwa na akili, ninyi mnishinde, yuko nani asiyeyajua mambo kama hayo? Mtu wa kuchekwa na wenziwe ni mimi, mimi niliyemwita Mungu, akaniitikia; kweli mwongofu asiyekosa kabisa ni mtu wa kuchekwa. Atesekaye hubezwa moyoni mwake naye akaaye na kutulia, yuko tayari kuwasukuma wajikwaao miguu. Mahema yao wapokonyi hutengemana, nao wamkasirishao Mungu hukaa na kutulia, ndio, Mungu anaowatia mengi mikononi mwao. Haya! Uliza nyama, wakufundishe, nao ndege wa angani, wakueleze! Au sema na nchi yenyewe, nayo itakufundisha! Hata samaki wa baharini watakusimulia mambo. Yuko nani asiyeyajua haya yote, ya kuwa mkono wa Mungu ndio ulioyatengeneza haya? Mkononi mwake zimo roho zao hao nyama wote, zimo nazo pumzi zao wote wenye miili ya kimtu. Sikio silo linaloyajaribu yanayosemwa, kama ufizi unavyovionja vyakula vyake? Werevu wa kweli uko kwao walio wazee, siku zikiwa nyingi, mtu hupata utambuzi. Werevu wa kweli na uwezo uko kwake Mungu, tena wongozi na utambuzi. Tazama: Akibomoa, hapajengwi tena; akimfunga mtu, hafunguliwi tena. Tazama: Akiyazuia maji, hukauka; tena akiyaachia huifudikiza nchi. Yeye ni mwenye nguvu na uwezo wa kufanya mambo, wake yeye ni apoteaye naye apotezaye. Wenye kukata mashauri huwapeleka kuwa mateka, nao waamuzi huwapumbaza. Mafungo ya wafalme huyafungua, tena huwafunga wenyewe kwa kamba viunoni pao. Nao watambikaji huwapeleka kuwa mateka, nao wenye nguvu huwaangamiza. Waliotegemewa kuwa mafundi wa kusema huwasemesha kibubu, nazo akili zao wazee huzipumbazisha. Huwamwagia mabezo walio wakuu, nao wenye nguvu huwalegeza mikanda. Huvumbua yaliyofichwa ndani ya nchi na kuyatoa gizani, nacho kivuli kiuacho hukitokeza mwangani. Hukweza mataifa, kisha huyaangamiza, hueneza mataifa mahali, kisha huyaacha, yatekwe. Wakuu wa makabila ya huku nchini huwatia kichaa, kisha huwapoteza nyikani pasipo na njia, wapapasepapase gizani pasipo na mwanga, huwaacha, wapepesuke kama mlevi. Tazameni! Jicho langu limeyaona hayo yote pia, sikio langu limeyasikia na kuyatambua. Mnayoyajua ninyi, nimeyajua ami, sikupungukiwa na akili, ninyi mnishinde. Kweli mimi na niseme naye Mwenyezi, napenda sana kujikania kwake Mungu. Kweli ninyi hutunga maneno yaliyo ya uwongo, nyote m waganga wasiofaa. Kama mngenyamaza kimya kabisa, mngejitokeza kuwa wenye werevu ulio wa kweli. Sikieni, jinsi ninavyojikania! Yategeni masikio, midomo yangu ikiyasema mashindano yangu! Je? Mtamtetea Mungu kwa kusema yaliyo mapotovu? Au mtamtetea kwa kusema yaliyo madanganyifu? Je? Mtampendelea Mungu kwa kumgombea magomvi yake? Je? Akiwachunguza ninyi, ingekuwa vema? Au mtaweza kumdanganyadanganya, kama watu wanavyodanganyana? Atawakemea kwa nguvu, mkipendelea watu na kufichaficha. Je? Utukufu wake hautawatia woga? Kitisho chake nacho hakitawaangukia ninyi? Makumbusho yenu ni mafumbo ya kijivu, nazo ngome zenu ni ngome za udongo. Ninyamazieni mimi, nipate kusema nami! Yatakayonijia na yanijie! Ingefaaje, nikiuma nyama za mwili wangu kwa meno yangu? Au nikiiweka roho yangu mikononi mwangu? Mtaona, akiniua; hakuna kingine, nikingojeacho; ninataka tu kumwelezea njia zangu usoni pake. Hili tu litasaidia kuniokoa, kwani mwovu hatokei usoni pake. Lisikilizeni vema neno langu, nayo maelezo yangu na yaingie masikioni mwenu! Tazameni! Nimelitengeneza shauri langu, najua, ya kuwa nitajitokeza kuwa asiyekosa. Yuko nani atakayebishana na mimi hapa? Kama yuko, ningenyamaza tu, nipate kuzimia. Haya mawili ninayataka, unifanyie, nisije kujificha usoni pako: uondoe mkono wako, usinilemee! Tena kizuie kitisho chako, kisinistushe! Kisha hapo, utakaponiita, mimi nitakuitikia! Au mimi niseme, nawe unijibu! Maovu yangu na makosa yangu, niliyoyafanya, ni mangapi? Nijulishe mapotovu yangu nayo makosa yangu! Mbona unauficha uso wako, ukaniwazia kuwa miongoni mwao wapingani wako? Utatetemesha jani lipeperushwalo? Au utakimbiza kibua kilicho kikavu? Kwani unaniandikia machungu kama haya, tena unanilipisha manza, nilizozikora nilipokuwa nikingali mwana. Nayo miguu yangu unaitia mikatale, ukapaangalia pote, nipitiapo, napo, nyayo za miguu yangu zinapokanyaga, unachora alama zako. Nami ninanyauka kama mwenye kibovu, nafanana na nguo iliyoliwa na nondo. *Mtu aliyezaliwa na mwanamke huwapo siku chache, nayo anayoyashiba ni mahangaiko tu. Huchanua kama ua, kisha hupukutika, hupita upesi kama kivuli, hakai. Ingawa awe hivyo, unayafumbua macho, kusudi yamlinde; lakini mimi unanipeleka shaurini, tusemeane huko. Miongoni mwao waliotoka kwa mwenye uchafu yuko atakataye? Hata mmoja tu hayuko. Mtu amekwisha kukatiwa siku zake, miezi yake imekwisha kuhesabiwa na wewe mwenyewe, umeiweka mipaka yake, asiipite.* Ikiwa hivyo, acha kumtazama, apate kupumzika, aifurahie hiyo siku yake kama mkibarua! Kwani kiko kingojeo kinachoupasa huo mti nao: kama unakatwa, huchipuka tena, nayo hayo machipukizi yake hayakomi. Mizizi yake ikioza nchini ndani, nalo shina lake likifa mchangani, kwa unyevu wa maji tu utachipuka tena, upate matawi sawasawa kama mche mpya. Lakini mtu akifa hutoweka, mwana wa Adamu akiisha kuzimia huenda wapi? Maji ya bahari hupwa, nayo ya mtoni hupotea kabisa, pawe pakavu. Vivyo hivyo naye mtu akija kulala hainuki tena; mpaka mbingu zitakapotoweka, hawaamki, wala hawataamshwa usingizini mwao. Laiti ungenificha kuzimuni, ukanilindia huko, mpaka yatulie makiali yako! Muda ulionikatia utakapokwisha pita, ungenikumbuka hapo! Mtu atarudi uzimani tena akiisha kufa? Kama ndivyo, ningengoja siku zangu zote za kushindana na mateso, mpaka nitakapopokelewa na mwenzangu mwingine. Hapo ningekuitikia, utakaponiita kwa kukitunukia kiumbe cha mikono yako. Sasa ukizihesabu nyayo zangu po pote, zilipokanyaga, makosa yangu nayo huyaangalii? Hapo maovu yangu yangefungiwa mfukoni na kutiwa muhuri, nazo manza zangu, nilizozikora, ungezifuta. Lakini sivyo; mlima ukianguka hutoweka, nao mwamba huondoka mahali pake, ulipokuwapo. Maji husaga mawe, yawe madogo, nayo mafuriko ya maji huuchukua mchanga wa nchi, hivyo nacho kingojeo cha mtu unakiangamiza. Unamshinda siku zote pia, ajiendee, unaugeuza uso wake ukimtuma kujiendea. Wanawe kama wanapata macheo, havijui; au kama wananyenyekezwa, hayatambui mambo yao. Huyasikia tu maumivu ya mwili wake yeye, nayo roho yake husikitika kwa ajili yake yeye. Elifazi wa Temani akajibu akisema: Yuko mwerevu wa kweli atakayejibu yenye ujuzi ulio kama upepo? Au yuko atakayelijaza tumbo lake upepo utokao maawioni kwa jua? Atamwonya mwenziwe kwa maneno yasiyofaa? Au atajisemea tu kwa mapuzi yasiyompatia mtu kitu? Kisha wewe unatangua kicho kiwacho chote, nayo mawazo ya kumnyenyekea Mungu unayabeua. Manza, ulizozikora, zinakifunza kinywa chako, ukachagua ulimi usemao yenye ujanja. Kinachokuumbua kuwa mwovu, si mimi, ni kinywa chako, nayo midomo yako ndiyo inayokusuta. Je? Mtu wa kwanza aliyezaliwa ni wewe? Au ulitoka tumboni mwa mama, milima ilipokuwa haijawa? Je? Ulizisikiliza njama za Mungu? Je? Ndiko, ulikouvuta werevu wa kweli, ukujie wewe? Unajua mambo gani, tusiyoyajua nasi? Unao utambuzi gani usiopatikana kwetu? Wenye mvi walio wazee nako kwetu sisi wako, siku zao ni nyingi sana kuliko hizo za baba yako. Je? Hivyo, Mungu anavyotuliza mioyo, unaviwazia kuwa vidogo? Nalo neno la upole si kitu kwako? Mbona moyo wako unakuchukua, ukupeleke penginepo? Mbona macho yako unayang'arisha hivyo? Inakuwaje, ukiigeuza roho yako, ije kumpingia Mungu, ukamtolea maneno kama hayo kinywani mwako? Mtu ndio nini, aweze kutakata? Aliyezaliwa na mwanamke awezaje kuongoka? Kumbuka hili tu: nao watakatifu wake hawezi kuwategemea, nazo mbingu hazitakati machoni pake! Sembuse mtu amchukizaye kwa upotevu, yeye mtu afanyaye maovu, kama ni kunywa maji tu! Nitakufunza, nisikilize! Niliyoyaona, na niyasimulie. Werevu wa kweli wanayoyatangaza ni yayo hayo, kwani waliyoambiwa na baba zao hawakuyasahau; walikuwa wamepewa nchi hii wao peke yao tu, wala hakuwako mgeni aliyepita kwao. Walisema: Asiyemcha Mungu hukaa siku zote na uchungu wake, vilevile mkorofi miaka yote, aliyowekewa na kuhesabiwa. Sauti za mastusho huingia masikioni mwake, akikaa na kutengemana, mwangamizaji humjia. Hayategemei, ya kwamba atatoka gizani, hujiwazia kuwa amechaguliwa kuuawa na upanga. Hutangatanga kujipatia chakula, lakini akione wapi? Anajua, ya kuwa kando yake imekwisha kuwekwa siku ya giza. Mateso na masongano humtia woga, nayo humshinda kwa nguvu kama za mfalme aliyejiweka tayari kupiga vita. Kwa kuwa ameukunjua mkono wake, ampingie Mungu, akajivunia kuwa mwenye uwezo mbele yake Mwenyezi. Akapiga mbio na kunyosha shingo, aje kumshinda, akijikingia ngao yake yenye vitovu Akaunonesha uso wake kuwa wenye mafuta, navyo viuno vyake akavinenepesha. Katika miji iliyotakiwa kuwa mahame ndimo, alimotua, akakaa katika nyumba, ambazo watu hawazikai, ndizo zinazongoja tu kuwa machungu ya mawe. Kwa hiyo hatapata mali nyingi, nazo atakazozipata hazitakaa, wala mazao yake hayatafurikia katika nchi hii. Hatapata kuondoka mle gizani, nayo machipukizi yake hukaushwa na ndimi za moto, naye atatoweshwa kwa nguvu za pumzi za kinywa chake Mungu. Asitegemee mambo yaliyo ya bure, maana atadanganyika, nayo yatakayokuwa malipo yake yatakuwa ya bure. Siku yake ikiwa haijatimia bado, hayo yatatimia, shina lake halitapata kabisa, litakapochipuka tena. Kama mizabibu inavyopukutisha mapooza yao, au kama michekele inavyopakatisha maua yao, hivyo utakuwa mlango wake ambezaye Mungu, utakosa wazao wo wote, nao moto utayala mahema yao waliowapenyezea watu. Mateso ndio mimba zao, kwa hiyo huzaa maovu, hivyo matumbo yao hutoa udanganyifu. Iyobu akajibu akisema: Maneno kama haya nimeyasikia mara nyingi, ninyi nyote mwatuliza moyo na kuusumbua! Maneno yaliyo kama upepo yamekwisha? Au kuna nini kinachokuchochea, ukinijibu hivyo? Mimi nami ningeweza kusema kama ninyi; kama roho zenu zingekuwa mahali pake roho yangu, nami ningeweza kukusanya maneno mazuri ya kuwaambia pamoja na kuwatingishia kichwa changu. Lakini kwa maneno ya kinywa changu ningewatia nguvu, nayo midomo yangu ingewatuliza mioyo kwa kuwakingia maovu. Lakini maumivu yangu hayazuiliki, ijapo niseme; tena kuna nini ninayopungukiwa, nikiacha kusema? Kwa kuuangamiza mlango wangu wote amenichokesha sasa. Wewe ukanikunjamanisha, upate ushahidi wa kunishinda, nako kukonda kwangu kwaniinukia, kunisute usoni pangu. Ukali wake ukaninyafua kwa kunionea tu, nayo meno yake huyatumia ya kunikerezea, akanikazia macho yake makali, yeye mpingani wangu. Wako wanaoniasamia vinywa vyao, wakanipiga mashavu na kunitukana, wote pia wakakusanyika kunijia mimi. Mungu akanifunga, kisha akanitoa, wao wanipotoe, akanitia mikononi mwao wasiomcha. Nalikaa na kutengemana, mara akaniponda, akanikamata shingoni, akanibwaga mwambani, kisha akanisimamisha tena, niwe shabaha yake. Wapigaji wake wa mishale wakanizunguka, wakanipasua mafigo yangu pasipo huruma, nayo maji yangu ya nyongo wakayamwaga chini. Kwa kunitia kidonda kwa kidonda akaniumiza vibaya, kama fundi wa vita akanijia na kupiga mbio sana. Gunia la kuifunika ngozi ya mwili wangu ndilo, nililojishonea, nayo pembe yangu nikaichomeka uvumbini. Uso wangu ukaiva sana kwa kulia, napo penye kope zangu kiko kivuli kama cha kifo. Tena mikononi mwangu hamna ukorofi, nayo maombo yangu hutakata. Usiifunike damu yangu, wewe nchi, wala malalamiko yangu yasipate kituo! Jueni: Hata sasa yuko shahidi wangu kule mbinguni, huko juu yuko atakayenitetea. Rafiki zangu wananifyoza, lakini macho yangu hivyo, yanavyojaa machozi, humtazamia Mungu. Yeye Mungu amwamulie mtu, ijapo ashindane naye, hata mwana wa Adamu akishindana na mwenzake, amkatie shauri. Kwani miaka imekwisha hesabiwa itakayokuja; nayo itakapokwisha, sina budi kuishika ile njia isiyo na kurudi. Roho yangu imenyongeka, siku zangu zinataka kuzimika, ni penye makaburi tu panaponingoja. Lakini na sasa yako masimango, wanayonitolea, nami sina budi kutazama tu kwa macho yangu, wakinitia uchungu. Nakuomba, jitoe mwenyewe kuniwia kole, kwani yuko wapi mwingine atakayepeana mikono na mimi? Kwa kuwa umeuficha ubingwa, usije mioyoni mwao, kwa hiyo hutawaacha tu, wajikuze wenyewe. Mtu akiwaalika wenziwe kugawanyiana fungu lake mwingine, ndipo, yatakapozimia macho yao wanawe huyo mtu. Aliyemweka kuwa fumbo la watu, ni mimi, mtu wa kutemewa mate usoni nitakuwa mimi. Kwa hiyo macho yangu yameingiwa kiwi kwa majonzi, navyo viungo vyangu vyote pia viko kama kivuli. Wanyokao wanayastuka sana mambo hayo, nao watakatao wanachafuka sana kwa ajili yao wambezao Mungu. Lakini mwenye kuishika njia yake ni mwongofu, naye mwenye mikono iliyo safi huongezeka nguvu. Lakini ninyi nyote rudini, mje kwangu, ingawa nisione aliye mwerevu wa kweli miongoni mwenu. Siku zangu zimekwisha kupita, mawazo yangu nayo yamekwisha kukatika, tena ndiyo yaliyokuwa mapato ya moyo wangu. Ingawa waugeuze usiku kuwa mchana, na kuniambia: Mwanga uko karibu kwako kuliko giza, nakungojea kuzimu tu kuwa nyumba yangu, nukitandikie malalo yangu kwenye giza. Kaburi sina budi kuliita: baba yangu ni wewe, navyo vidudu: mama yangu na maumbu zangu. Kwa hiyo kingojeo changu kingine kiko wapi? kilicho kingojeo changu, yuko nani atakayekichungulia? Nacho kitashuka kufika penye makomeo ya kuzimu; ndiko, tutakakotulia pamoja uvumbini. Bildadi wa Sua akajibu akisema: Hata lini mtatanda matanzi, yanase maneno? Itambueni maana, kisha tusemeane! Tukiwaziwa kuwa kama nyama, ni kwa sababu gani? Mbona tunawaziwa kuwa wenye uchafu machoni penu? Wewe unajirarua mwenyewe kwa ukali wako? Je? Kwa ajili yako wewe nchi itaachwa, isikae mtu? Au mwamba utaondoka mahali, ulipokuwa? Kweli mwanga wake asiyemcha Mungu utazima, nazo cheche za moto wake hazitaangaza. Mwanga utakuwa giza hemani mwake, nacho kinara chake kilichomo kitazima. Miguu yake iliyokwenda kwa nguvu itasongeka, mashauri yake, aliyowapa wengine, yatambwaga chini. Kwani atanaswa miguu yake kwa wavu akitembea penye matanzi yaliyofichwa. Itakayokikamata kisigino chake ni kamba, itamshika kwa nguvu, mtambo ukifyatuka. Kitanzi cha kumnasia kimefichwa mchangani, hata njiani amewekewa mtego wa kumkamatia. Vitisho humstusha po pote na kuitia miguu yake woga, ikimbie sana. Mabaya yanayomtaka ni yenye njaa ya kumla, mwangamizo uko tayari, upate kumwangusha, utavila viungo vya kuungia mwili ngozini mwake; mwana wa kwanza wa kifo atavila kweli hivyo viungo vyake. Atatolewa kwa nguvu hemani mwake, alimokimbilia, aendeshwe kufika kwake mfalme aliye mwenye mastusho. Hemani mwake watakaa wasio wa ukoo wake, nayo mawe ya kiberiti yatamwagwa juu ya kao lake. Chini mizizi yake itakauka, hata juu matawi yake yatanyauka. Ukumbuko wake utapotea, utoweke huku nchini, hatakuwa kabisa na sifa yo yote kwao walioko nje. Watamkumba, atoke mwangani, aje gizani, watamfukuza, atoke kabisa humu ulimwenguni. Hatakuwa na mwana wala mjukuu katika ukoo wake, wala hatakuwako atakayesalia katika makao yake. Siku yake wataistukia sana watakaotokea nyuma, kama wao waliokuwa mbele walivyokufa ganzi. Hayo ndiyo yatakayoyapata makao ya mpotovu napo mahali pake yeye asiyemjua Mungu. Iyobu akajibu akisema: Roho yangu mtaisikitisha mpaka lini kwa kujisemea maneno tu ya kuniumiza? Sasa ni mara kumi, mkinitukana; lakini kwa kunihangaisha hivyo hamwoni soni? Itakapotokea kuwa kweli, ya kama nimekosa, mimi ndiye, litakayemkalia hilo kosa langu. Kama mnajikuza kweli na kunibeua, kama mimi ni mtu apaswaye na kutwezwa, haya! Niumbueni! Jueni, ya kuwa ndiye Mungu aliyenipotoa kwa kunitegea pande zote tanzi lake. Tazameni! Nikiulilia ukorofi sijibiwi, wala hakuna aniamuliaye, nikilalamika. Njia yangu ameifunga kwa kitalu, nisipitie hapo, napo penye mikondo yangu amepapatia giza. Yaliyokuwa utukufu wangu amenivua, nacho kilemba amekiondoa kichwani pangu. Kwa sababu amenibomolea pande zote, sina budi kujiendea, nacho kingojeo changu ameking'oa, kama ni mti tu. Akanitolea makali yake, yaniwakie moto, akaniwazia kuwa kama mmoja wao wapingani wake. Vikosi vyake vikaja, vikutanie pamoja, vikajitengenezea njia ya kufika kwangu, vikayapiga makambi yao, yanizunguke hemani mwangu. Ndugu zangu akawaweka mbali, wasije kwangu, nao wenzangu wa kujuana nao wakanigeukia kuwa kama wageni. Walio wa ukoo wangu nao wakapotea, nao rafiki zangu wema wakanisahau. Waliokaa pamoja na watumishi wa kike nyumbani mwangu wao ndio wanaoniwazia kuwa mgeni, machoni pao nikageuka kuwa mtu asiye wa kwao. Nikimwita mtumishi wangu, haitikii, sharti nimwambie maneno mengi ya kumbembeleza. Pumzi zangu zinamchukia mke wangu, mnuko wangu mbaya unawachukia, niliowazaa mwenyewe. Nao walio vijana bado hunibezabeza, nikiinuka, husema maneno ya kunifyoza. Wote waliokuwa wenzangu wa njama wanachukizwa na mimi, nao waliogeuka kuwa wapingani wangu ndio, niliowapenda. Ngozi na nyama za mwili wangu zinagandamana na mifupa, kilichopona kwangu ni ufizi tu. Nihurumieni, nihurumieni, ninyi wenzangu! Kwani mkono wa Mungu umenipiga. Mbona mnanikimbiza kama Mungu, msishibe kuzinyafuanyafua nyama za mwili wangu? Laiti maneno yangu yangeandikwa kwa kupigwa chapa kitabuni! Laiti yangechorwa namo mwambani kwa kalamu ya chuma, kisha kutiwe risasi, yawepo kale na kale! Mimi ninayoyajua ndiyo haya: Mkombozi wangu yupo, ni mwenye uzima, naye huko mwisho ndiye atakayeinuka uvumbini. Mwili wangu wenye ngozi utakapokwisha kuharibika, huu mwili wangu wenye nyama utakapokuwa haupo, hapo ndipo, nitakapopata kumwona Mungu; mimi mwenyewe nitamwona kuwa wangu, macho yangu ndiyo yatakayomwona, siyo ya mgeni tu; mafigo yangu yanazimia ndani yangu kwa kuyatunukia hayo. Mkisema: Haya! Na tumkimbize! kwani mizizi ya mambo haya imeonekana kwangu: uogopeni upanga rohoni mwenu! Kwani kutoa makali yenye moto hutupatia hukumu za upanga; zitakapotokea, ndipo, mtakapojua: mapatilizo yako! Sofari wa Nama akajibu akisema: Kwa sababu hii mawazo yangu yananishurutisha, nikujibu, maana ninachafuka sana moyoni mwangu. Ninasikia maneno ya kunikanya, nayo ya kunitukana, lakini kwa utambuzi wangu ninajibiwa mengine rohoni mwangu. Je? Hayo huyajui tangu kale, tangu hapo, watu walipokaa katika nchi? Ya kuwa shangwe zao wasiomcha Mungu hukoma upesi? Ya kuwa furaha ya mwovu hukaa kitambo kidogo tu? Ijapo ayakuze majivuno yake, yafike mbinguni, kichwa chake kiyaguse nayo mawingu, hupotelea kale na kale kama mavi yake, waliomwona waulize: yuko wapi? Hupita kwa kuruka kama ndoto, watu wasimwone tena, hufukuzwa kama ono baya la usiku. Jicho lililomchungulia halitomwona tena, wala mahali pake, alipokuwa, hapatamtazama tena. Wanawe watabembeleza walio wanyonge, mikono yao itazirudisha mali, alizozinyang'anya. Ijapo, mifupa yake izidi kuwa nazo nguvu za ujana, lakini haina budi kulala pamoja naye uvumbini. Kama anauona ubaya kuwa mtamu kinywani mwake, aufiche, upate kukaa chini ya ulimi wake, autunze vizuri, asitake kuuachilia, ujiendee, ila auzuie, usiondoke penye ufizi wake: kisha hicho chakula chake kitageuzwa tumboni mwake kuwa uchungu wa pili mle ndani yake; hizo mali nyingi, alizozimeza, hana budi kuzitapika, Mungu akizitoa kwa nguvu tumboni mwake. Kwa hivyo, alivyonyonya sumu iliyo ya pili, mwisho ulimi wa moma utamwua, asijifurahishe tena kwa kuvitazama vile vijito wala ile mito inayokwenda na kujaa asali na mafuta. Aliyoyasumbukia hana budi kuyarudisha, hawezi kuyameza, ijapo mapato yake yawe mengi mno, hayafurahii. Kwani alipokwisha kuwaponda wanyonge, aliwaacha papo hapo, akanyang'anya nyumba, asizozijenga. Lakini hakujua kutulia ndani yake yeye; kwa hiyo hatapona pamoja nayo, aliyoyatunukia. Kwa ulafi wake hakikuwako kitu, asichokichukua; kwa sababu hii hivyo vyema vyake havikai kabisa. Hapo atakapofurikiwa, ndipo, atakaposongeka, mikono yao walioteswa naye ikimjia yote. Ndipo, Mungu atakapolijaza tumbo lake akituma kwake makali yake yawakayo moto, ayanyeshe juu yake yampatie chakula cha kushiba. Itakapokuwa, ayakimbie mata ya chuma, uta wa shaba utampiga, achomwe; akitaka kuutoa mshale, utakuwa umetokea mgongoni pake, chembe yake imetukayo itakuwa imeichoma nayo nyongo; basi, mastusho yatamjia vivyo hivyo. Mambo yote ya giza yako tayari kwake kuviangamiza vilimbiko, nao moto uwakao pasipo kupulizwa utamla mwenyewe, nayo yaliyosalia hemani mwake utayamaliza. Mbingu zitazifunua manza, alizozikora, nayo nchi itainuka kumshinda shaurini. Nyumba yake iliyompatia yatatekwa, yatakuwa kama maji yakaukayo, siku ya ukali wake Mungu itakapotimia. Hilo ndilo fungu, mtu asiyemcha Mungu atakalolipata kwake Mungu, ndio urithi, atakaogawiwa naye Mungu. Iyobu akajibu akisema: Sikieni na kulisikiliza neno langu! Hili litakuwa la kuituliza mioyo yenu. Niacheni, nipate kusema mimi nami! Nitakapokwisha kuyasema yangu, na msimange tena. Je? Yuko mtu, ninayemsuta? Mbona sishindwi na kuvumilia? Nigeukieni mimi, mpate kustuka na kuiweka mikono vinywani mwenu! Kweli nami nikiyakumbuka nashikwa na woga, mwili wangu nao unakufa ganzi. Mbona wasiomcha Mungu huwapo? Mbona huwa wazee, nguvu zao zikiendelea kuongezeka? Vizazi vyao huviona kwao kwa macho yao kuwa vyenye nguvu, nao wajukuu wao wako machoni pao. Nyumba zao hukaa salama pasipo kustushwa, nayo fimbo ya Mungu haiwapigi. Ng'ombe wao waume huzaza vema pasipo kukosa, ng'ombe wao wake huzaa vizuri pasipo kuharibu mimba. Huwatembeza watoto wao walio wengi kama kundi la kondoo, nao vijana wao huchezacheza na kupaza sauti wakiimbia patu na mazeze na kuifurahia milio ya mazomari. Siku zao huzitumia za kula mema, kisha hushuka kuzimuni kwa mara moja. Nao humwambia Mungu: Ondoka kwetu! hatupendezwi kuzijua njia zako. Mwenyezi ni nani, tumtumikie? Inatufaliaje kumtokea na kumwomba? Lakini tazameni: mema yao hawayashiki mikononi mwao, kwa hiyo mashauri yao wasiomcha Mungu na yanikalie mbali! Taa zao wasiomcha Mungu zikizima, ni mara ngapi? Si kila mara, unapowajia mwangamizo wao? Ni mara ngapi, Mungu akiwapatia matanzi kwa kuwakasirikia, wawe kama bua kavu penye upepo au kama makapi, yakipokonywa na upepo wa chamchela? Mwasema: Mungu huwawekea watoto wao maovu yao; lakini angewalipisha wenyewe, wapate kumjua, macho yao wenyewe yangeuona mwangamizo wao, wakinyweshwa makali yake Mwenyezi yaliyo yenye moto. Kwani mlango wao unawezaje kuwapendeza huko nyuma yao, miezi yao ikiisha kukatwa kwa kuitimiza hesabu yao? Je? Wanataka kumfundisha Mungu, apate kuwajua? Naye ndiye awahukumuye nao walioko huko juu. Huwa hivi: mmoja anakufa mwenye nguvu zake zote, naye alikuwa anatengemana na kutulia kabisa, vyombo vyake vya kukamulia vikijaa maziwa, kiini cha mifupa yake nacho kikiwa chenye mafuta. Mwingine anakufa mwenye uchungu rohoni mwake, kwa kuwa hakuna chema cho chote, alichokila. Kisha hulala pamoja humo uvumbini, vidudu vikiwafunika wote wawili. Tazameni! Ninayajua mawazo yenu nayo mashauri yenu ya kunikorofisha. Mwasema: Nyumba ya mkuu aliyetesa watu iko wapi? Mahema, wasiomcha Mungu waliomokaa, yako wapi nayo? Je? Wapitao njiani hamkuwauliza hayo? Hamzitambui habari zao za mambo, waliyoyaona wao? Kwamba: Siku ya msiba mbaya hupona, siku, makali yanapotokea, huepuka. Yuko nani anayeziumbua njia zake usoni pake? Tena yuko nani anayemlipisha aliyoyafanya yeye? Naye husindikizwa mpaka mazikoni, tena kaburini kwake wanangoja zamu. Udongo wa bondeni anauona kuwa mtamu, watu wote wanamfuata nyuma yake, nao waliomtangulia hawahesabiki. Nanyi mnaniambiaje matulizo ya moyo yaliyo ya bure? Kwani yanayosalia ya majibu yenu, ni ukatavu tu. Elifazi wa Temani akajibu akisema: Mtu anayeweza kumfalia Mungu yuko wapi? Kwani mwenye akili hujifalia mwenyewe tu. Itampendeza Mwenyezi, ukiwa mwongofu? Anapata nini, ukizitengeneza njia zako, zisikukoseshe? Je? Anakupatiliza kwa kumwogopa? Hii ndiyo sababu ya kukupeleka shaurini? Siyo mabaya yako yaliyo mengi? Hakuna kikomo cha manza, unazozikora. Kwani ndugu zako uliwatoza rehani bure tu, nao wakosao nguo ukawavua mavazi. Mwenye kiu hukumpa maji, apate kunywa, naye mwenye njaa ukamnyima chakula. Aliyekuwa mwenye mkono, nchi ikawa yake, naye aliyejivuna usoni pa watu ndiye aliyepata kukaa huku. Wajane uliwafukuza kwako, wajiendee mikono mitupu, nao waliofiwa na wazazi wakaumizwa mikono. Kwa hiyo sasa matanzi yanakuzunguka pande zote, mara yanafyatuka, yakutie woga. Au hiyo giza nayo huioni? Wala furiko la maji litakalokufunika? Je? Mungu hayuko mbinguni juu? Zitazame nazo nyota zilizoko mbali juu ya kichwa chako! Nawe unasema: Mungu anayoyajua ndio nini? Akiwa mawinguni mwenye weusi atawezaje kutuamua? Hujificha mle mawinguni, asione kitu; hutembea na kuzunguka mbinguni tu. Je? Unaiangalia njia ya kale, usiiache? Nao walioikanyaga ni watu waovu. Siku zao zilipokuwa hazijatimia bado, ndipo, walipopokonywa, msingi wao ulipoyeyuka kuwa kama jito; ndio, waliomwambia Mungu: Ondoka kwetu! Yako mambo gani atakayotufanyizia huyo Mwenyezi? Naye ndiye aliyezijaza nyumba zao vitu vyema; kwa hiyo mawazo yao wasiomcha na yawe mbali, yasinifikie! Waongofu wakiyaona watafurahi, naye atakataye atawasimanga kwamba: Kumbe waliotuinukia wametoweka, nayo masao yao moto umeyala! Jizoeze kuandamana naye Mungu, upate kutengemana! Mema yake yatakavyokufikia, ndivyo hivyo. Kinywa chake kikikuonya, mwitikie, nayo maneno yake yaweke moyoni mwako! Utakaporudi kwake Mwenyezi utajengwa, ni hapo, utakapoutoa upotovu mahemani mwako, usikukaribie tena. Huo mchanga wenye dhahabu uutupe uvumbini, nayo dhahabu ya Ofiri itupe penye vijiwe vya mito! Ndipo, Mwenyezi atakapokuwa dhahabu zako na fedha zako zipitazo nyingine kwa kima kikuu. Hapo ndipo, utakapomfurahia aliye Mwenyezi na kumwelekezea Mungu uso wako. Utakapomlalamikia, atakusikia, nawe utayalipa uliyoyaapa, umtolee yayo hayo. Nalo utakalowaza kulifanya, utafanikiwa, hata katika njia zako mwanga utakumulikia. Zitakapokunyenyekeza, utasema: Na nitukuke, naye aliye mnyenyekevu machoni pake mwenyewe atamwokoa. Naye asiyetakata atamponya, kweli atapona kwa mikono yako, ikiwa imetakata. Iyobu akajibu, akisema: Je? Hata leo maombolezo yangu ni kumkataa Mungu? Kwani mkono wangu umelemea kwa kupiga kite. Ninatamani kuijua njia ya kumwona, nifike hapo, anapokaa. Ningemwelezea shauri langu, alijue, nikakijaza kinywa changu maneno ya kushindana naye. Ningejua maneno, atakayonijibu, na kuyatambua, atakayoniambia. Je? Kwa nguvu zake nyingi angenigombeza? Sivyo, mwenyewe angeniangalia na kunisikia. Hapo ningeshindwa naye kwa kunyoka, nikapona kale na kale mikononi mwake anihukumuye. Lakini nikienda upande wa maawioni kwa jua, hayuko; wala upande wa machweoni kwa jua simwoni, wala kushotoni, kama yuko katika kazi zake, simpati, tutazamane; wala kuumeni simwoni, sijui, alikogeukia. Lakini anaijua njia, niliyoishika: kama angenijaribu, ningetokea nikitakata kama dhahabu. Kwani miguu yangu imeshika njia ya kuzifuata nyayo zake yeye, nikaiangalia hiyo njia yake, nisiiache. Sikurudi nyuma na kuliacha agizo la midomo yake, maneno ya kinywa chake nikayaangalia kuliko maongozi yangu. Lakini yeye alivyo, ndivyo alivyo, yuko nani awezaye kumgeuza? nayo roho yake inayoyataka kweli, huyafanya. Hivyo atayatimiliza nayo, aliyoyaagiza, yanipate mimi; yako mengi yaliyomo moyoni mwake kama hayo. Kwa hiyo nitastuka, nitakapomwona, nashikwa na woga naye nikijaribu kumtambua. Mungu ameutisha moyo wangu, yeye Mwenyezi akanistusha. Kwani kwa kuogopa giza sizimii, wala kwa kuliona giza lenye weusi, jinsi lilivyonifunika. Mbona hazikuwekwa na Mwenyezi siku zake za mapatilizo? Mbona hawazioni hizo siku zake wao wamjuao? Wasogezao mipaka wako huku, nao wanyang'anyao makundi ya kondoo, wayachunge kuwa yao. Punda wao waliofiwa na wazazi huwachukua, nao ng'ombe wa wajane huwakamata kuwa rehani. Huwakumba maskini, waondoke njiani, wanyonge wa huku chini wote pia hawana budi kujificha. Watazameni, kama hawafanani nao vihongwe vya nyikani: hutoka na mapema kufanya kazi zao za kujipatia chakula, wanakojipatia chakula cha watoto, ndiko porini. Mashambani kwa watu huchuma ya kujilisha, nayo mizabibu yao wasiomcha Mungu huiokoteza. Hulala usiku wenye uchi pasipo nguo za kujifunika, hawana mablanketi ya kujizuilia baridi ya kipupwe. Hulowa kwa kunyewa na mvua za milimani, kwa kukosa kimbilio hujibana mwambani. Tena wako wapokonyao kifuani kwa mama waliofiwa na baba, nao wanyonge huwavua mavazi kuwa rehani; kisha huwaacha, wajiendee wenye uchi pasipo nguo yo yote; nao wenye njaa huchukuzwa viganda vya ngano. Uani pa mabwana zao hutengeneza mafuta, ijapo wenyewe wawe wenye kiu, huwakamulia wao zabibu. Wenye kufa wakipiga kite, husikilika toka mjini, nazo roho zao waliouawa kwa nguvu hulilia malipizo, lakini wakipumbazwa vibaya hivyo, Mungu haviangalii. Wenye kuchukizwa na mwanga ndio wenzao wale, hukataa kuzitambua njia zake hivyo, zilivyo, penye mikondo yake hawakai. Mwuaji huinuka, kukipambazuka, aje kumwua mnyonge naye mkiwa, mambo ya usiku hufanana nayo yake mwizi. Macho ya mzinzi hungoja kuchwa kwa kwamba: Pasipatikane jicho litakaloniona; kwa hiyo huuficha uso wake. Penye giza hujipenyeza nyumbani mwa watu, kwa kukataa kuona mwanga hujifungia mchana. Mapema yao hao wote pamoja ndio giza kuu, kwani huvijua mastusho yake hilo giza kuu. Yeye kwa kuwa kama aendaye juu ya maji laiti angepita upesi, fungu lake la huku chini liapizwe, njia ya kwenda mizabibuni asiishike tena! Kama kiangazi kinavyotowesha maji ya theluji kwa ukali wa jua, vivyo hivyo kuzimu na kuwatoweshe wakosaji walio hivyo. Nalo tumbo la mama na limsahau, wadudu wakiufurahia utamu wa mwili wake; kwa kuwa mpotovu na avunjwe kama mti, asikumbukwe tena. Kwa maana aliwanyang'anya vyao wanawake wasiozaa, nao wajane hakuwafanyizia chema cho chote. Kwa uwezo wake Mungu huwakalisha sana walio wenye nguvu, hata aliyekwisha kukata tamaa ainuke tena na kupata uzima. Humpa kukaa na kutulia kwa kupata egemeo, nayo macho yake huzielekea njia zao. Wakiisha kujipatia utukufu mara hawako tena, hutoweka kwa kupokonywa kama wote wengine; nao hukatwa kama masuke yaliyoko juu mabuani. Au sivyo vilivyo? Yuko nani awezaye kuniumbua kuwa mwongo na kuyatokeza maneno yangu kuwa ya bure? Bildadi wa Sua akajibu akisema: Utawalaji na utisho uko kwake anayepatengemanisha pake palipo huko juu. Je? Vikosi vyake vinahesabika? Yuko nani asiyetokewa na mwanga wake? Kwa hiyo mtu atawezaje kuwa mwongofu machoni pake Mungu? Aliyezaliwa na mwanamke atawezaje kutakata? Ukiutazama mwezi utauona: hauangazi kabisa, wala nyota hazitakati machoni pake. Sembuse mtu aliye dudu! Sembuse mwana wa Adamu aliye funyo! Iyobu akajibu akisema: Kweli umemsaidia sana asiye na uwezo, ukamwokoa mwenye mikono isiyo na nguvu! Asiyeerevuka kweli umemwongoza vema ukimjulisha mizungu iliyo mingi! Ni nani, uliyemwambia hayo maneno yako? Tena ni roho ya nani iliyokusemesha? Nao wazimu walioko chini hutetemeka, nayo maji pamoja nao wakaao humo. Kuzimu kuko waziwazi machoni pake, huko ndani ya nchi hakuna kabisa ficho lo lote. Aliutandaza upande wa kaskazini mahali pasipokuwa na kitu, nayo nchi aliiweka kuwa juu ya hapo pasipokuwa lo lote kabisa. Katika mawingu yake hufunga maji, lakini hakuna wingu lipasukalo chini yao. Hukifunika kiti chake cha kifalme, kisionekane, kwa kukitandazia wingu lake. Alipima mviringo juu ya maji, uwe mpaka; ndipo, mwanga unapokutana nayo giza. Nguzo za mbingu hutukutika kwa kutetemeka, akichafuka. Kwa uwezo wake huzistusha nazo bahari, kwa utambuzi wake huwaponda nao nondo waliomo baharini. Kwa kuzipuzia mbingu huzichangamsha, mkono wake humchoma naye joka kubwa, akikimbia. Tazameni! Huku ni kama pembeni tu kwa njia zake, hayo maneno yake, tunayoyasikia, ni manong'ono tu, lakini hizo nguvu za ngurumo zenyewe yuko nani atakayezitambua? Iyobu akaendelea kutoa mifano akisema: Hivyo, Mungu alivyo Mwenye uzima, ijapo akatae kuniamulia, hivyo, Mwenyezi alivyoitia roho yangu machungu haya, siku zote, nitakapokuwa ninakokota roho bado, pumzi ya Mungu itakapokuwa ingalimo puani mwangu: midomo yangu haitasema neno lipotokalo, wala ulimi wangu hautaongopa. Ninyi sitawaitikia kale na kale mpaka nitakapozimia, sitakoma kuvieleza kwamba: Sikukosa. Neno hili ninalishika sana, sitaliacha kwamba: Mimi ni mwongofu, moyo wangu haunisutii moja tu miongoni mwao siku zangu. Mchukivu wangu na yampate yanayompata asiyemcha Mungu, naye aniinukiaye na yampate yaleyale yanayompata mpotovu. Kwani mwovu akijipatia mapato kwa kukorofisha watu, Mungu atakapoitaka roho yake kwake, yuko na kingojeo gani? Mungu atavisikia vilio vyake, masongano yatakapompata? Au atamfurahia Mwenyezi, amlilie Mungu kila, anapotaka? Nitawafundisha ninyi matendo yake mkono wa Mungu, Mwenyezi anayoyafanya, sitawaficha! Ninyi nyote yatazameni mliyoyaona! mbona mwajisemea tena maneno yaliyo bure kabisa? Hili ni fungu lake asiyemcha Mungu lililoko kwake Mungu, tena ni urithi, watakaoupata kwake Mwenyezi, wao wakorofi. Wanawe watakapokua watauawa na upanga, nao wajukuu wake hawatashiba vyakula. Watakaosalia kwake watazikwa kwa kuuawa na kipindupindu, nao wajane wao hawatawaombolezea. Ijapo, alimbike fedha kuwa nyingi kama mavumbi, ijapo, ajiwekee mavazi kuwa mengi kama mchanga, ijapo, ayaweke hivyo, atakayeyavaa ni mwongofu, nazo fedha watajigawanyia wao watakatao. Akijenga nyumba yake, huwa kama buibui, au kama dungu, wanalomjengea mlinzi. Anakwenda kulala mwenye mali, lakini ni mara ya mwisho, akifumbua macho, hakuna mali tena. Mastusho yanamfikia kama maji mengi, upepo wa chamchela unampokonya usiku. Upepo utokao maawioni kwa jua unamchukua, ajiendee, ukimwondoa kwa nguvu hapo pake, alipokuwa. Unampiga mishale yake pasipo kumhurumia, hata atake hili mojo tu: kukimbia, atoke mkononi mwake. Watu wanampigia makofi na kumzomea, akitoka hapo pake, alipokuwa. Fedha zina mahali pao zinapoonekana, nazo dhahabu zina mahali pao, wanapozifulia mitoni. Vyuma vinachimbuliwa uvumbini, tena yako mawe yanayotokea shaba kwa kuyeyushwa. Nalo giza mtu analikatia mpaka, ayachunguze mawe yaliyoko kule kuliko na giza lenyewe kwenye mlango wa kuzimu. Huko anachimbua shimo refu sana, kisha nayo njia ya ndani ya nchi pasipokaa watu; wanawahauliwa kwa kuwa chini ya hapo, watu wanapokanyaga; ndiko, wanakojiangika na kuning'inia, watu wengine wakiwa mbali. Nchi itoayo chakula juu chini yake inafudikizwa kwa kuchimbuliwa na nguvu zilizo sawa nazo za moto. Mahali pamojamoja huonekana mawe yenye almasi, pengine nayo madongo yenye dhahabu. Naye tai haijui njia hiyo, wala macho ya kozi hayajaiona kwa kuchungulia. Nyama wakali wenye majivuno hawajaikanyaga, wala simba mwenyewe hajaishika. Nayo mawe magumu yenyewe mtu huyavunja kwa mkono wake, hata milima anaifudikiza kwa kuichimbua toka misingini. Miambani anachonga njia za kupitia ndani yao; ndivyo, macho yake yanavyoona yote yaliyo yenye kima. Vijito vya ndani anaviziba, visimchuruzikie maji, apate kuyatokeza mwangani yaliyofichika ndani ya nchi. Lakini werevu wa kweli unaonekana wapi? napo mahali penye utambuzi pako wapi? Hakuna mtu ajuaye, unapotengenezwa, hauonekani katika nchi yao wenye uzima. Vilindi husema: Kwetu sisi hauko, nayo bahari husema: mimi nami sinao. Hata kwa dhahabu safi haupatikani, wala haulipiki kwa fedha kuwa bei yake, wala haupimiki kwa dhahabu tupu ile ya Ofiri, wala kwa almasi au kwa vito vya sardio vilivyo vyenye kima. Wala dhahabu wala vioo vizuri mno ndivyo vinavyolingana nao, wala haununuliki kwa vyombo vya dhahabu vyenye urembo. Marijani na ulanga uangazikao vizuri hayakumbukwi uliko, kuwa na werevu wa kweli ni mali kuliko lulu. Hauwezekani kulinganishwa navyo vito vya topasio vitokavyo Nubi, wala haupimiki kwa dhahabu itakatayo kabisa. Je? Werevu wa kweli unatoka wapi? napo mahali penye utambuzi pako wapi? Umefichika machoni pao wote walio wenye uzima, nao ndege wa angani hawauoni, kwa kuwa uko umefunikwa. Kuzimu nacho kifo husema: Kwa masikio yetu tulisikia tu, ukitajwa. Mungu anaitambua njia ya kwenda kwake, yeye tu anapajua, hapo pake ulipo. Kwani yeye huchungulia hata mapeoni kwa nchi, huyaona yaliyoko chini ya mbingu. Alipoutengeneza ukali wa upepo, alipoupima wingi wa maji, alipoyatengeneza maongozi ya mvua nayo njia ya umeme ulio wenye ngurumo: hapo ndipo, alipouona, kisha akautangaza kwa watu, akaushikiza, akauchunguza. Kisha akawaambia watu: Tazameni! Kumcha Bwana ndio werevu wa kweli, kuyaepuka mabaya ndio utambuzi. Iyobu akaendelea kutoa mifano akisema: Laiti ningekuwa, kama nilivyokuwa katika miezi iliyopita, Mungu alipoziangalia siku zangu! Hapo taa yake ilimulika juu ya kichwa changu, kwa mwanga wake nikaenda hata gizani. Siku zile nilikuwa mwenye nguvu za kiume, Mungu naye akakaa hemani mwangu kuwa mwenzangu wa mashauri. Hapo Mwenyezi alikuwa pamoja na mimi, nao watoto wangu wakanizunguka. Hapo miguu yangu ilioshwa kwa maziwa, nao mwamba uliochuruzika vijito vya mafuta ulikuwa kwangu. Nilipotokea langoni kwenye mji, nikiweke kiti changu uwanjani, vijana waliponiona wakaondoka kwenda pengine, nao wazee wakainuka, wasimame; Wakuu wakayakomesha maneno yao na kuviweka viganja vinywani mwao. Sauti za mabwana wakubwa nazo zikanyamaza, ndimi zao zikagandamana na fizi zao. Sikio la mtu liliponisikia, akanishangilia, jicho la mtu liliponiona, akanishuhudia. Kwani nilimponya mnyonge, aliponililia, hata waliofiwa na wazazi, walipokosa msaidiaji. Mbaraka yake aliyeufikia mwangamizo ikanijia, nayo mioyo ya wajane nikaichangamsha. Nilivaa wongofu, uniwie nguo, nayo maamuzi yangu yakawa kama kanzu na kilemba. Kipofu nilikuwa macho yake, kiwete nilikuwa miguu yake. Maskini mimi nilikuwa baba yao, nalo shauri la mtu, nisiyemjua, nikalichunguza vema. Lakini mpotovu nilimvunja meno, namo mlemle katika meno yake nikayapokonya aliyoyanyang'anya. Kwa hiyo nilisema: Katika kiota changu ndimo, nitakamozimia, siku zangu zitakapokuwa nyingi kama za mtende. Mizizi yangu itatandama juu penye maji, nao umande utayanyea matawi yangu usiku kucha. Utukufu, nilio nao, utakuwa mpya kila siku, nao upindi wangu utajipatia nguvu mpya mkononi mwangu. Mimi watu walinisikiliza na kungoja, nimalize; nilipowapa shauri langu, wakaninyamazia. Hakuwako mwingine aliyesema, nilipokwisha kusema, maneno yangu yakawa kama matone yaliyowadondokea. Kama wanavyongoja mvua, ndivyo, walivyoningoja, vinywa vyao vikaasama kama vyao wanaotwetea mvua ya vuli. Walipotaka kukata tamaa, nikawachekea, hawakuweza kuuinamisha chini uso wangu, ulipoangaza. Nilipojielekeza kwenda kwao nilikaa nao kama kichwa chao, au kama mfalme katika vikosi vyake kwa kuwa kama mtu anayewatuliza mioyo waliosikitika. Sasa wananicheka walio wenye siku chache kuliko mimi, ambao baba zao nilikataa kuwaweka mahali, mbwa wa makundi yangu ya kondoo walipokuwa nao. Nazo nguvu za mikono yao zingenifalia nini? Kwani uwezo wao wenye nguvu ulikuwa umeangamia. Kwa kuwa ukosefu na njaa zilikuwa ziliwagofua, huguguna nayo mazao ya nyika iliyo kama jangwa jeusi, iliyo tupu kabisa pasipo cho chote cha kulisha watu. Kwa hiyo huchuma vijanijani vyenye chumvi panapo na vichakachaka, nayo mizizi ya mifagio ni chakula chao. Hufukuzwa penye watu wengine, wakiwazomea kama wezi. Hawana budi kukaa katika makorongo yaogopeshayo, hata mashimoni ndani ya nchi, hata miambani. Hulia kwa njaa vichakani wakilala chini ya upupu. Ndio wenye upumbavu wenyewe wasiojua hata majina yao, nako kwao walifukuzwa na kupigwa. Sasa nimegeuka kuwa mtu wao hao wa kumzomea, nikapata kuwa kwao kama fumbo. Kwa kutapishwa na mimi huwa mbali, wasinifikie karibu, lakini hawajikatazi kunitemea mate usoni pangu. Vilivyowazuia wakavifungua, wanitese, usoni pangu wakavitupa mbali hivyo vifungo vyao. Hawa watu waovu hujisimamisha kuumeni kwangu, waisukume miguu yangu, iondoke kwao, nazo njia zao zilizowaangamiza hunitwika mimi. Njia yangu wakaichimbua, isipitike, wao wakosao msaidiaji husaidia kunitumbukiza mwangamizoni. Kama ni kutokea katika ufa mpana, hunijia mimi, makelele yao huzidi sana kwa kusukumana. Mastusho kama hayo yakanigeukia, kama ni kwa nguvu za upepo yakautangua ukuu wangu upesi, nayo yawezayo kuniokoa yakatoweka kama wingu. Kwa hiyo roho yangu imeyeyuka sasa ndani yangu, siku za kuteseka zikanipata. Usiku unaichoma mifupa yangu huko ndani, mpaka ioze, nayo maumivu yangu yanayoniguguna hayapumziki. Hizo nguvu nyingi zikaligeuza vazi langu, zikanikaza kama ukosi wa kanzu yangu. Zikanibwaga matopeni, nikafanana nayo mavumbini na majivu. Nikikulilia, wewe, hunijibu; hata nikisimama, unanitazama tu. Umegeuka kuwa mpingani wangu asiyenihurumia, kwa huo uwezo wa mkono wako ukanifukuza. Ukaniinua na kuniweka juu ya upepo, unipeleke, ukaniyeyusha kwa hizo nguvu za chamchela. Nakujua, utakakonipeleka, ndiko kufani, uniingize nyumbani mwenye mkutano wao wote waliokuwa uzimani. Je? Mtu akitumbukia shimoni hanyoshi mkono? Au mtu akizama hapigi yowe kwa sababu hiyo? Aliyepatwa na siku ngumu sikulia naye? Roho yangu haikumsikitikia naye mkiwa? Nilipotazamia mema, mabaya yakaja; nilipongojea mwanga, giza ikaja. Matumbo yakachafuka, yakakataa kunyamaza, siku za mateso ziliponifikia mimi nami. Nikajiendea na msiba wangu pasipo kuona jua, nikaondoka penye mkutano, nipate kulia. Nimegeuka kuwa ndugu yao mbwa wa mwitu, na mwenzao mumbi wapigao kite. Ngozi yangu inachubuka kwa kuwa nyeusi, itoke mwilini mwangu, nayo mifupa yangu imeungua kwa joto la mwili. Hivyo zeze langu limegeuka kuwa la kuombolezea, nalo zomari langu hupiga sauti za vilio tu. Nilifanya agano na macho yangu, kisha ningewezaje kumtazama mwanamwali kwa kumtamani? Kwani Mungu huko juu angalinipatia nini? Yeye Mwenyezi angalitoa fungu gani mbinguni, liwe langu? Je? Wapotovu fungu lao sio mwangamizo? Nao wafanyao maovu fungu lao sio machukivu? Yeye hazioni hizo njia zangu? Wala hazihesabu nyayo zangu? Kama nilifanya mwenendo ulio wa uwongo, miguu yangu ikakimbilia yaliyo madanganyifu, Mungu na anipime kwa mizani iliyo sawa; ndipo, atakapojua, ya kuwa sikukosa. Kama nyayo zangu ziliiacha njia yake, kama moyo wangu ulizifuata tamaa za macho yangu, kama uchafu wo wote uligandamana na mikono yangu: basi, mimi nitakayoyapanda, mwingine na ayale, nayo mazao yangu na yang'olewe pamoja na mizizi yao! Kama moyo wangu uliingiwa na tamaa ya mke wa mwingine, mpaka nikaja kumwotea mlangoni pake mwenzangu, mke wangu na amsagie mwingine unga wake, hata wengine na waje kulala naye. Kwani hili lingekuwa kosa lililo baya zaidi, ni kukora manza zipasazo kuhukumiwa na waamuzi wakuu. Hivyo ningalijipatia moto wa kunila hata kuzimuni, nao ungaliyaangamiza yote pia, niliyoyapata. Kama nilikataa shauri la mtumishi wangu wa kiume au wa kike, walipotaka kushindana na mimi mwenyewe, ningefanya nini, Mungu akininukia? au ningemjibu nini, akiyakagua? Je? Aliyenitengeneza tumboni mwa mama hakumtengeneza naye? Siye yeye mmoja aliyetuumba kuwa mimba? Wanyonge niliwanyima walichokitaka kwangu? Au nilizimisha macho yaliyokuwa ya mjane? Au nililila tonge langu peke yangu, afiwaye na wazazi asile naye? Sivyo, ila tangu ujana wangu alikulia kwangu kama kwa baba yake, toka hapo nilipotoka tumboni mwa mama yangu niliwaongoza wajane. Hapo nilipoona mtu, akifa kwa kukosa nguo, au maskini akikosa lo lote la kujifunika, basi, viuno vyake havikunibariki, alipojipatia kijoto kwa nguo za nywele za kondoo wangu? Kama nilikemea mwana aliyefiwa na wazazi nikimkunjulia mkono kwa kuona wanaonisaidia langoni penye mashauri, bega langu na lianguke kwa kuteuka mahali pake, nalo fupa la mkono wangu na livunjike kiungoni mwake! Kwani mwangamizo wa Mungu ungalinistusha, nisiweze kusema neno kwa hivyo, anavyotukuka. Kama nilitumia dhahabu kuwa egemeo langu, na kuziwazia zile dhahabu safi kuwa kimbilio langu, kama niliufurahia wingi wa mali zangu, kwa kuwa mkono wangu ulipata vingi vya kuvilimbika, kama hapo, nilipolitazama jua, jinsi linavyoangaza, au mwezi, jinsi unavyoendelea ukiwa na utukufu wake, kama hapo moyo wangu huko ndani ulitamani kutambika, mpaka kinywa changu kikakinonea kiganja changu: huko ningekora manza zipasazo kuhukumiwa na waamuzi wakuu, kwani huko ningemkana Mungu wa huko juu kuwa Mungu wangu. Je? Nilimfurahia mchukivu wangu, alipoteswa? Au nilishangilia, mabaya yalipompata? Sikukipa kinywa changu ruhusa kukosa hivyo, kije kuiapiza roho yake, ishuke kuzimuni. Walioingia hemani mwangu hawasemi: Yuko mtu asiyeshibishwa na nyama, alizompa? Kweli kwangu hakuwako mgeni aliyelala nje, mimi humfungulia mpitaji milango yangu. Je? Niliyafunika mapotovu yangu kama watu wengine? Au nilizificha manza, nilizozikora, kifuani pangu? Je? Pako, nilipoogopa wingi wa watu? Au yalinistusha mazomeo ya milango yao, hata nikanyamaza, nisitoke nyumbani? Kama ningepata mtu atakayenisikiliza, ningemwonyesha maandiko yangu, Mwenyezi anijibu. Kiko nacho kitabu, alichokiandika mwenye kunigombeza; kweli hicho ningekichukua begani pangu, au ningekifunga kichwani pangu kuwa kilemba changu. Ningemsimulia hesabu ya nyayo zangu, tena ningekuwa kama mkuu wa watu, nimkaribie. Kama shamba langu linanisuta na kupiga kelele, kama matuta yake yanaitikia na kulia, kama niliyala mazao yake pasipo kulipa na kuizimisha roho yake mwenye shamba, basi, penye ngano na patokee mangugi matupu, napo penye mawele ndago tu! Maneno, Iyobu aliyoyasema, yamekwisha. Hao watu watatu walipoacha kumjibu Iyobu, kwa kuwa alikuwa mwongofu machoni pake, ndipo, makali ya Elihu wa Buzi, mwana wa Barakeli wa mlango wa Ramu, yalipowaka moto, naye Iyobu ndiye, makali yake yaliyemwakia, kwa kuwa alijiwazia rohoni mwake kuwa hakumkosea Mungu. Nao wale wenzake watatu makali yake yakawawakia, kwa kuwa hawakuona tena la kumjibu Iyobu la kumwumbua kuwa amekosa. Lakini Elihu alikawia kusema na Iyobu, kwani wale walikuwa wakubwa kumpita yeye kwa siku zao. Elihu alipoona, ya kuwa hakuna jibu tena litokalo vinywani mwao wale watatu, makali yake yakawaka kama moto. Ndipo, Elihu wa Buzi, mwana wa Barakeli, alipojibu, akasema: Mimi ni mdogo kwa miaka, ninyi m wazee, kwa hiyo nimejizuia, nikaogopa kuwaelezea ninyi, ninayoyajua mimi. Nilisema: Wenye uzee na waseme, walio na miaka mingi na waujulishe werevu wa kweli. Lakini kinachowapa watu utambuzi ni roho iliyomo mwao pamoja na pumzi yake yeye Mwenyezi. Lakini wazee wenye miaka mingi sio wanaoerevuka kweli, wao wazee sio wanaoyajua mashauri yaliyo sawa. Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni, mimi nami niyaeleze, ninayoyajua! Tazameni! Nimeyangojea maneno yenu, nikausikiliza utambuzi wenu, mlipouchunguza, mvumbue, hayo mambo yalivyo. Ninyi nimewaangalia sana, hii ni kweli; lakini nilipotazama sikumwona aliyemshinda Iyobu, wala mmoja wenu hakuweza kumjibu aliyoyasema. Msiseme: Kwa kuwa ni mwenye werevu wa kweli, tumeona, atakayemshinda ni Mungu, si mtu. Hajajiweka tayari kusema na mimi, lakini kama ninyi mlivyosemeana naye, sitamjibu hivyo. Ndipo, walipostuka, hawakujibu tena, wakawa wamepotelewa na maneno ya kusema. Walipokuwa hawasemi neno, nikangoja, lakini wakasimama tu pasipo kujibu tena. Basi, nami na nijibu fungu langu, nami na niyaeleze, ninayoyajua. Kwani nimejaa maneno ya kusema, roho yangu humu ndani yangu imesongeka, mpaka niyatoe. Tazameni: Tumbo langu linafanana na mvinyo isiyofunguliwa njia, ni kama viriba vipya vinavyotaka kupasuka. Na niseme, humu ndani mpanuke kidogo tu, na niifumbue midomo yangu, nijibu nami. Sitaki kupendelea uso wa mtu, wala maneno yaliyo mafuta ya midomo tu sitamwambia mtu, kwani yaliyo mafuta ya midomo tu sijui kuyasema, muumbaji wangu angeniondoa upesi sana. Kwa hiyo Iyobu, yasikilize nitakayoyasema! Maneno yangu yote yategee masikio yako! Tazama! Nitakifumbua kinywa changu, ulimi wangu useme kinywani mwangu. Maneno yangu yananyoka kama moyo wangu; midomo yangu itayasema ninayoyajua, yaliyo ya kweli. Roho ya Mungu aliyeniumba na pumzi ya Mwenyezi zinanipa kuwapo. Kama utaweza na unijibu! Jiweke tayari kusimama usoni pangu! Tazama! Mimi na wewe kwake Mungu tu sawa, mimi nami nilifinyangwa kwa udongo. Tazama! Sikutishi, usinistukie, nayo nitakayokutwika yasikulemeze. Kweli ulisema masikioni pangu, nikaisikia sauti yao hayo maneno: Ninatakata, sikufanya kiovu, mimi ni safi, sikukora manza. Tazama! Yako mambo, Mungu aliyonionea: ananiwazia kuwa miongoni mwao wachukivu wake. Anaitia miguu yangu mikatale, anapaangalia pote, nipitapo. Tazama! Ninakujibu: kwa hiyo huongoki, kwani Mungu ni mkuu kuliko mtu. Mbona unamgombeza kwa kusema: Hayo yote hajibu neno liwalo lote? Lakini Mungu akisema mara moja au mara mbili, mtu haangalii; au sivyo? Watu wakiona ndoto kwa kulala usiku wenye usingizi mwingi, hapo, wanapokuwa wanalala vitandani pao, ndipo, anapoyazibua masikio ya watu, ayatie muhuri hayo, aliyowafunza na kuwaonya, amkataze mtu kuyafanya tena, aliyoyafanya, ayakinge majivuno, yasimpate mtu; aizuie nayo roho yake, isitumbukie shimoni, nao mwili wake wenye uzima, usipite penye mishale iuayo. Kwa hiyo mtu anachapwa na kuumizwa kitandani pake, mifupa yake ikishindana na mateso pasipo kukoma. Huchafukwa na moyo anapokula, ijapo kiwe chakula hicho, anachokitamani rohoni. Nyama za mwili wake zinakauka, zisionekane, mifupa yake iliyokuwa haionekani ikatokea waziwazi. Roho yake ikafika karibu kuingia shimoni, nao moyo wake ukawafikia wauuao. Hapo malaika akamtokea, ampatanishe na Mungu, mmoja wao walioko kama elfu; akimwonyesha mtu njia ya kunyoka tena, ndipo, atakapomhurumia na kumwambia: Mwokoe huyu, asishuke shimoni! Kwani makombozi yake nimeyapata. Ndipo, nyama za mwili wake zitakapochipuka kuliko zile za utoto, azirudie kuwa kama siku hizo za ujana wake. Atakapomwomba Mungu, atapendezwa naye, atamwonyesha uso wake, aushangilie; ndivyo, anavyompatia mtu kuwa mwongofu tena. Naye ataimba, watu wamsikie, akiungama kwamba: Nalikosa kwa kuyapotoa yanyokayo, lakini hakuna malipo, niliyotozwa! Akaikomboa roho yangu, isitumbukie shimoni, moyo wangu uufurahie huu mwanga! Tazama! Hayo yote ndiyo, Mungu anayoyafanya mara mbili, hata mara tatu, airudishe roho ya mtu, isitumbukie shimoni, mwanga wenye uzima umwangazikie. Tega masikio, Iyobu, unisikilize! Nyamaza tu, mimi niseme! Kama unaona la kusema, nijibu! Sema! Kwani nitapendezwa kukuona kuwa mwenye wongofu. Kama wewe huna la kusema, nisikilize! Nyamaza tu, nikufunze werevu ulio wa kweli! Elihu akajibu tena akisema: Mlio werevu wa kweli, yasikieni ninayoyasema! Nitegeeni masikio yenu, mlio wajuzi! Kwani sikio huyajaribu yanayosemwa, ufizi nao huyaonja yanayoliwa. Yaliyo sawa ndiyo, tujichagulie, sote pamoja tuyajue yaliyo mema! Kwani Iyobu amesema: Mimi sikukosa, lakini Mungu ananinyima shauri lililo sawa. Ingawa sikukosa, napewa uwongo, kidonda, mshale wake ulichonipiga, hakiponi, tena hakuna kiovu, nilichokifanya. Mtu aliye kama Iyobu yuko wapi? Masimango ya kwake yakichuruzika kama maji ya kunywa, akifanya bia nao wafanyao maovu, akitembea na watu wasiomcha Mungu? Kwani amesema: Hakuna mafaa, mtu anayojipatia kwa kupendezana naye Mungu. Kwa hiyo nisikilizeni, ninyi waume mlio wenye akili! Mungu asiwaziwe kamwe ya kwamba: Hufanya maovu, wala Mwenyezi ya kwamba: Hufanya mapotovu! Ila humlipisha mtu matendo yake, aone yaupasayo mwenendo wake. Hii ni kweli, Mungu hafanyi maovu, wala Mwenyezi hayapotoi mashauri yaliyo sawa. Kuiangalia nchi hii alimwagiza nani? Au yuko nani aliyeuweka huu ulimwengu wote? Kama angeuelekeza moyo wake kuyaangalia yamfaliayo mwenyewe, au kama angeirudisha kwake roho na pumzi yake, wote wenye miili yenye nyama wangezimia kwa mara moja, nao watu wangerudi kuwa mavumbi tena. Kama uko na utambuzi, yasikilize haya! Itegee sauti ya maneno yangu masikio yako! Je? Achukizwaye na mashauri yaliyo sawa anaweza kutawala? Au mkuu aongokaye utamwazia kuwa mwovu? Utamwambia mfalme: Hufai kitu? au wakuu: M waovu? Naye Mungu hazipendelei nyuso za wakuu, wala hawatazami wenye nguvu kuliko wanyonge, kwani wote ni viumbe vya mikono yake. Punde si punde, mara watu hufa, usiku wa manane hupepesuka, kisha huenda zao, nao wenye nguvu huondolewa pasipo kushikwa mikono. Kwani macho yake huziangalia njia za watu, nyayo zao zinapokanyaga, hupaona pote. Hapapatikani penye giza kabisa wala kivuli chenye weusi, wapate kujificha mlemle wafanyao maovu. Kwani Mungu hamwangalii mtu mara kwa mara akimtaka, aje kwake kukatwa shauri. Huvunja wenye nguvu pasipo kuwachunguzachunguza, akaweka wengine mahali pao. Kwani anazijua kazi zao, zilivyo kweli, akawakumba usiku, wapondwe. Kwa kuwa ni waovu, huwapiga mahali palipo na watu wanaovitazama. Ni kwa sababu waliacha kumfuata, nazo njia zake zote hawakuziangalia, wazishike. Huko ni kuwatwika vilio vyao wakorofikao, navyo vilio vya wanyonge, alivyovisikia. Akiwanyamazisha hivyo, yuko nani atakayemwambia: Unafanya nini? Akiuficha uso wake, yuko nani awezaye kumwona? Njia yake ya kuwaendea wote ni hiyo moja, wao walio mataifa mazima naye mtu aliye peke yake. Huku ni kwamba: Mtu mpotovu asiwe mfalme, asigeuke kuwa tanzi la kutegea watu. Je? Mungu anaambiwa: Nalipishwa, lakini sikukosa? Kama yako, nisiyoyaona, nifundishe wewe! Kama nilifanya mapotovu, sitayafanya tena? Je? Kama inavyokupendeza wewe, ndivyo alipishe? Unavikataaje? Ni wewe upaswaye kuchagua malipo, siye yeye? Haya! Yaseme unayoyajua! Watu wenye akili wataniambia pamoja na waume walio werevu wa kweli wanaonisikia: Iyobu aliyoyasema siyo ya ujuzi, kweli maneno yake siyo ya mtu mwenye akili. Basi, kwa hiyo Iyobu na ajaribiwe kale na kale, kwani kama watu waovu wanavyojibu, ndivyo, anavyojibu naye. Kwani makosa yake anayaongeza na kufanya maovu, akitupigia makofi machoni petu, tena akimgombeza Mungu kwa kusema kwake. Elihu akajibu tena akisema: Je? Hayo unayawaza kuwa shauri likupasalo, ukisema: Mimi ni mwenye wongofu kuliko Mungu? tena ukiuliza, kama huo wongofu utakupatia faida gani, tena ukisema: Nikiacha kukosa, inafaaje kuliko kukosa? Mimi nitakujibu wewe nao wenzako walioko kwako: Zitazame mbingu, upate kuona! Yaangalie mawingu yaliyoko huko juu kichwani pako! Yule unamtendea nini ukikosa? Mapotovu yako yakiwa mengi, unamfanyizia nini? Yule unampa nini usipokosa? Au liko, atakalolichukua mkononi mwako? Uovu wako utaweza kumwumiza mtu tu aliye kama wewe, nao wongofu wako utaweza kumfalia mwana wa Adamu. Kwa wingi wa mateso watu hulia, kwa kutolewa nguvu na wakuu hupiga makelele. Lakini hakuna aulizaye: Yuko wapi Mungu aliyeniumba? Siye anayeniimbisha hata usiku? Atufundishaye kuliko nyama wa porini siye yeye? Tena siye yeye atuerevushaye kuliko ndege wa angani? Lakini asipojibu, wanapomlilia, ni kwa ajili ya majivuno yao walio wabaya. Vilio vya bure Mungu havisikii, aliye Mwenyezi haviangalii. Ikiwa, unasema nawe, ya kama humwoni, hilo shauri liko kwake, wewe umngoje tu! Makali yake yasipotokea hata sasa, huwaziwa kuwa hajui kabisa, mtu akikorofishwa. Naye Iyobu amekifunua kinywa chake, vikawa vya bure, amesema maneno mengi ya mambo, asiyoyajua. Elihu akajibu tena akisema: Ningoje kidogo, nikueleze mambo! Kwani yako mengine ya Mungu, nitakayoyasema. Haya, ninayoyajua, niliyatoa mbali, nimtokeze yeye aliyenifanya kuwa mwenye wongofu. Kweli maneno yangu siyo ya uwongo, anayesema na wewe ni mwenye ujuzi utimilikao. Tazama! Mungu ni mwenye uwezo, lakini hamtupi mtu, ni mwenye uwezo kwa nguvu zilizo za moyo. Hamkalishi uzimani asiyemcha, lakini watesekao huwakatia mashauri yaliyo sawa. Kwake mwongofu hayaondoi macho yake, anawakalisha pamoja na wafalme katika viti vya kifalme, wakae hapo kale na kale, wapate kutukuka. Lakini walipofungwa kwa mapingu, au walipokamatwa kwa kamba za mateso, ndipo, anapowaelezea matendo yao, wayaone, jinsi yalivyo, huwaonyesha mapotovu yao, waliyoyafanya kwa kujikuza. Hapo huwafunulia masikio, wasikie, akiwaonya, na kuwaambia, warudi na kuyaacha maovu yao, akiwatisha. Ikiwa, wanamsikia, waje kumtumikia, ndipo, watakapozimaliza siku zao na kuona mema, nayo miaka yao na kuifurahia; wengine sharti wapite penye mishale iuayo, ndio wasiomsikia; kwa kukosa ujuzi watazimia. Ndipo, wenye mioyo mipotovu watakapokasirika, lakini hawatajipa mioyo ya kupiga kelele, ya kuwa aliwafunga. Hivyo roho zao zitakufa katika ujana wao, nayo mioyo yao huzimia kwao wagoni. Lakini watesekao huwaponya katika mateso yao, akawafunua masikio kwa kuwasonga. Wewe nawe anakutaka, akuopoe katika masongano, akuweke papana pasipokusonga, nawe uandaliwe yenye mafuta mengi mezani pako. Lakini ukizidi kuzitamani hukumu zao wasiomcha Mungu. basi, hukumu zao na mashauri yao yatakupata kweli. Angalia, ukali usikuponze, ukitukana, wala wingi wa makombozi usikupoteze! Je? Makelele yako yatakupatia mahali pasiposongeka, ijapo, ujikaze kulia kwa nguvu zote? Usikutwetee kuchwa, kuwe usiku! Kwani ndio unaomaliza makabila mazima, yatoweke mahali pao. Jiangalie mwenyewe, usiyageukie maovu! Kwani ndiyo, unayoyapenda kuliko mateso. Tazama! Mungu hufanya makuu kwa nguvu zake, yuko nani awezaye kufundisha kama yeye? Yuko nani amwagizaye kuzishika njia zake yeye? Au yuko nani awezaye kumwambia: unafanya mapotovu? Usisahau kuyatukuza matendo yake, watu wanayoyaimbia! Watu wote huyatazamia na kuyachunguzia, yangaliko mbali. Tazama! Mungu ni mkuu, tusimjue hivyo, alivyo, hesabu ya miaka yake haichunguziki. Huvuta matone ya maji, yaje juu kuwa kungugu, kisha hugeuka kuwa mvua idondokayo chini; ndivyo, mawingu yanavyoichuruzisha, inyeshee watu wengi. Je? Yuko anayeyatambua matandazo ya mawingu? Au makao yake, ngurumo zitokamo? Tazama! Huutandaza umeme wake, umzunguke, navyo vilindi vya bahari huvifunika. Hivyo ndivyo, anavyoyapatiliza makabila ya watu, tena ndivyo, anavyowapa watu vyakula, viwe vingi mno. Mikono yote miwili huifunika kwa umeme, akauagizia wao, utakaowapiga. Ngurumo zake ndizo zinazoujulisha, akichafuka kwa kumkasirikia amwinukiaye. Kweli moyo wangu nao huyastukia hayo, ukakupuka mahali pake, ulipokuwa. Ngurumo za sauti yake zisikilizeni vema, nayo mavumi yanayotoka kinywani mwake! Huzifungua, zienee po pote chini ya mbingu, nao umeme wake huufikisha nako mapeoni kwa nchi. Sauti yake hunguruma, ukiisha kuwapo; ndipo, unapoivumisha hiyo sauti yake yenye utukufu; kusudi sauti yake ipate kusikilika, hauzuii umeme. Mungu akiivumisha sauti yake, inastaajabisha; hufanya makuu, tusiyoweza kuyajua. Kwani huiambia kungugu: Anguka chini! nayo manyunyu huyafanya kuwa mvua, kisha hizo mvua huzitia nguvu zake, zinyeshe sana. Hizo huizuia mikono ya watu wote kufanya kazi, wote pia wayajue matendo yake. Hapo nao nyama huenda kujificha, watulie mapangoni mwao, ndimo, wanamotaka kukaa. Chamchela hutoka chumbani mwake huko kusini, nako kaskazini hutoka upepo wenye baridi ufukuzao mawingu. Kwa pumzi ya Mungu hutokea barafu, nayo maji yaliyopanuka hugandamana. Hata mawingu huyalemeza kwa kuyatia maji mengi, yaanguke chini, tena hutandaza nayo mawingu yenye umeme wake. Naye huyaongoza, yageuke huko na huko kuzifanya kazi zao, atakazoyaagiza, zitendeke huku chini po pote panapokaa watu; kama anataka kuipiga nchi yake au kuihurumia, kila mara huyapeleka papo hapo, anapoyatakia kazi. Haya yasikilize, wewe Iyobu, upate kuyatambua vema mastaajabu ya Mungu! Jinsi Mungu anavyoyaagiza, unavijua? au jinsi anavyoumulikisha umeme ulioko mawinguni kwake? Je? Unayajua mawingu, jinsi yanavyoning'inia? Mastaajabu yake, aliyotimiza kuyajua yote, unayatambua nawe? Nguo zako hazikuwashi joto, wewe mtu, nchi ikitulia kwa jasho litokalo kusini? Je? Unaweza kuzitandaza mbingu kama yeye, ziwe kama kioo cha shaba kwa kushupaa hivyo? Haya! Na utujulishe tutakayomwambia! Sisi hatuwezi kuyatunga kwa kuwa gizani. Je? Atapashwa habari ya kwamba: Nataka kusema? Yuko mtu aliyesema, aangamizwe? Mwanga wa jua, likiwaka mbinguni, watu hawawezi kuutazama, upepo ukiisha kupita na kuyaondoa mawingu, pang'ae tena. Kaskazini hutokea mionzi ya jua imetukayo kama dhahabu, kweli utukufu wake Mungu huogopesha. Sisi hatukumwona Mwenyezi kwa kuwa mkuu mwenye nguvu, hapotoi shauri wala mambo yo yote yaongokayo. Kwa hiyo inapasa, watu wamwogope, hawatazami watu wo wote wajiwaziao kuwa werevu wa kweli. Ndipo, Bwana alipomjia Iyobu akiwa mwenye upepo wa kuvuma na nguvu, akasema: Ni nani huyu ayatiaye giza matengenezo yangu akijisemea maneno yakosayo ujuzi? Haya! Jifunge viuno vyako kama mtu wa kiume! Kisha nitakuuliza, unijulishe mambo. Nilipoiweka misingi ya nchi, ulikuwa wapi? Kama unajua utambuzi, ieleze! Ni nani aliyeviweka vipimo vyake? Sema, kama unavijua! Au ni nani aliyeipima kwa kamba ya kupimia? Misingi yake ilikochimbiwa, ndiko wapi? Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni, zilipopiga shangwe nyota za mapema zote pamoja, nao wote waliokuwa wana wa Mungu walipopiga vigelegele? Ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, ilipotoka tumboni mwa nchi kwa kufurika? Nilipoipatia mawingu kuwa mavazi yake ka kungu jeusi kuwa nguo zake za kujitandia? Nilipoipinga kwa kuishurutisha kuyafuata maongozi yangu, napo nilipoiwekea makomeo na milango kuwa mipaka? Nilipoiambia: Ufike mpaka hapa, usipapite! Ndipo, mawimbi yako yenye majivuno yatakapokomea? Tangu hapo, siku zako zilipoanza, uliagiza, kuche, ukayajulisha mapambazuko mahali pao pa kutokea, yapate kuyashika mapeo ya nchi, waovu wafukuzwe, waitoke nchi? Hapo nchi hugeuka kama udongo, ukichorwa marembo, vyote vikijipanga kuwa kama mavazi yake mazuri mno. Lakini wanaonyimwa mwanga wao ndio waovu, nayo mikono iliyokunjuliwa kwa majivuno huvunjwa. Penye matokeo ya bahari ulipafika? Ukatembea humo ndani ya bahari mlimo na vilindi? Malango ya kifo yakafunguka mbele yako? Nayo malango ya kuzimu ukayaona? Ukapata kuutambua nao upana wa nchi? Kama unaujua wote, haya! Ueleze! Njia ya kwenda huko, mwanga unakokaa, iko wapi? napo mahali pake giza pako wapi? Unaweza kuisindikiza, uipeleke kwake? Njia za kwenda nyumbani kwake unazijua? Kweli unazijua! Kwani hapo ulikuwa umekwisha kuzaliwa, nayo hesabu ya siku zako ni kubwa! Penye vilimbiko vya theluji ulipafika? Navyo vilimbiko vya mvua ya mawe uliviona? Siku za masongano ndizo, nilizoviwekea, hata siku ya magombano nayo ya mapigano. Njia ya kwenda hapo, mwanga unapogawanyika, iko wapi? Upepo wa maawioni kwa jua unatoka wapi, uenee juu ya nchi? Ni nani azichimbiaye mvua mifereji, zikifurika? Tena ni nani, auelekezeaye umeme njia yake, ukinguruma? Ni nani ainyesheaye mvua hiyo nchi isiyokaa watu, nako kusikopatikana wana wa Adamu, kule nyikani? Ni nani atakayelishibisha jangwa napo palipo patupu kabisa, apachipuze na kuotesha majanijani? Je? Baba ya mvua yuko wapi? Ayazaaye matone ya umande ni nani? Tumboni mwa nani ndimo, barafu inamotoka? Tena ni nani auzaaye umande wa theluji, utoke mbinguni? Ni kazi ya nani, maji yakipata mafuniko kama ya mawe, nayo maji ya vilindi yakishikamana huko juu kwa kugandamanishwa? Je? Mafungo ya zile nyota saba za Kilimia unaweza kuyafunga? au kuyafungua mapingu yao zile nyota tatu za Choma, nikuchome? Je? Utazitoa nyota za Mviringo wa Nyama kila moja wakati wake? au zile za Gari na za watoto wake utaziongoza? Je? Maongozi ya mbinguni unayajua? au ni wewe unayezipa nchi hii, ziitawale? Je? Unaweza kuzipaza sauti zako, zifike mawinguni, uite mvua yenye maji mengi, ije kukufunika? Je? Unaweza kuutuma umeme, uende mahali fulani, kisha ukuambie: Mimi hapa! Nimerudi! Ni nani afanyaye yenye ujuzi kama hayo pasipo kujulikana? Au ni nani ayatambulishaye kwao wayachunguzao? Ni nani awezaye kuyahesabu mawingu, asipotelewe? Au ni nani awezaye kuvimwaga viriba vya mbinguni, mavumbi yashikamane kuwa udongo wa chepechepe, nayo mengine yageuke kuwa matope yagandamanayo? Je? Unaweza kumpokonya simba mke nyama, aliyemrarua? Au unaweza kuikomesha njaa ya wana wa simba, wakiwa mapangoni mwao, waotame, au wakikaa mafichoni na kuvizia? Ni nani awapatiaye makunguru vilaji vyao, wana wao wakimlilia Mungu na kutangatanga kwa kukosa chakula? Je? Unajua wakati, minde wanapozalia, au umeangalia, majike ya kulungu wanapopatia mimba? Miezi yao ya kuwa wenye mimba umekwisha kuihesabu? Tena unajua wakati, wanapozalia? Huchutama, kisha huwazaa watoto wao, huko ndiko kuukomesha uchungu wao. Watoto wao hupata nguvu kwa kukua penye mapori matupu; wakijiendea na kutoka kwao hawarudi tena. Ni nani aliyewatuma punda milia kujiendea tu? au ni nani aliyeyafungua mafungo yao vihongwe? Si mimi niliyewapa nyika kuwa nyumba zao nalo jangwa la chumvi kuwa makao yao? Wao huyacheka makelele yaliyomo mijini, maana hawazisikii tena sauti za ukorofi za wasimamizi. Milimani ndiko, wanakojionea malisho yao, vijani vibichi vyote huvifuatafuata. Je? Nyati atapendezwa akikutumikia? Atatafuta kilalo cha kuwamo zizini mwako? Je? Unaweza kumfunga nyati kwa kamba, akulimie matuta, akikufuata na kulivuta jembe mabondeni pako? Kwa kuwa nguvu zake ni nyingi, unaweza kumwegemea, umwachie kazi zako za shambani? Atayapeleka mazao yako nyumbani, ukimtegemea hivyo? Au yaliyomo chanjani mwako atayakusanya vema? Mabawa ya mbuni huchezacheza, lakini je? Hayo mabawa na manyoya yake yako na upole? Kwani mayai yake huyaacha hapo mchangani, huo mchanga uyaangue kwa joto lake; husahau, ya kama labda mguu utapapita utakaoyakanyaga, au nyama wa porini atayapondaponda. Watoto wake huwakuza kwa ukali, kama sio wake, haogopi kwamba: Labda hautafaa huo utunzaji wake. Kwani Mungu humsahaulisha werevu wa kweli, wala hakumgawia utambuzi wo wote. Lakini anapoyapigapiga mabawa yake, aondoke, humcheka naye farasi pamoja naye ampandaye. Je? Ni wewe uliyempa farasi nguvu zake kubwa? Je? Ni wewe uliyemvika singa za shingoni? Je? Ni wewe unayemtuma, aogopeshe watu akiruka kwa mara moja kama nzige na kufoka sana? Huparapara bondeni akizifurahia nguvu zake, hutoka kwenda kukutana nao washikao mata. Hucheka waoga, maana hastuki, wala penye panga harudi nyuma. Podo hupiga kelele juu yake, nayo mikuki imetukayo pamoja na chembe za mishale. Akichafuka kwa ukali humeza nchi, baragumu likilia, hasimami, ila kila anapolisikia baragumu husema: Haya! Toka mbali hunusa, mapigano yaliko, akiyasikia matangazo ya wakuu na makelele ya vikosi. Je? Ni kwa utambuzi wako kipanga akiruka angani na kuyanyosha mabawa yake kwenda kusini? Au ni kwa agizo lako, tai akipaa juu sana na kujitengenezea kiota cha mahali palipo juu? Hutua penye miamba, apate kulala magengeni juu; ngome yake ilipo, ndipo papo hapo. Toka huko juu huchungulia akitafuta chakula, macho yake huyaona nayo yaliyoko mbali. Makinda yake hufyonza damu, napo panapo nyamafu yupo hapo. Bwana akamjibu Iyobu akisema: Je? Mgombezaji atabishana naye Mwenyezi? Atakayebishana na Mungu na ajibu! Ndipo, Iyobu alipomjibu Bwana akisema: Mimi ni mdogo zaidi, nikujibu nini? Nimekifumba kinywa changu kwa kiganja changu. Nimesema mara moja, lakini sitajibu tena, sitaendelea kusema mara ya pili. Bwana akamjibu Iyobu akiwa mle upeponi mwenye nguvu za kuvuma, akasema: Haya! Jifunge viuno vyako kama mtu wa kiume! Kisha nitakuuliza, upate kunijulisha! Je? Mashauri, niliyoyakata, utayatangua wewe? Je? Utaniumbua kuwa mwovu, ujitokeze kuwa mwongofu? Je? Uko na mkono kama wake Mungu? Kwa kupaza sauti utaweza kunguruma kama yeye? Haya! Jipambe utukufu na ukuu! Jivike urembo na enzi! Yamwage machafuko ya ukali wako, mbwage chini kila, utakayemwona, ya kuwa amejivuna! Kila utakayemwona, ya kuwa amejivuna, umnyenyekeze! Nao waovu waangushe papo hapo, wanaposimama! Wachimbie uvumbini wote pamoja, nazo nyuso zao zifungie gizani hapo, wanapochimbiwa! Ndipo, nitakapokutukuza mimi nami kwa kwamba: Mkono wako wa kiume unakuokoa. Mtazame kiboko, niliyemwumba, kama nilivyokuumba wewe; naye hula majani kama ng'ombe. Zitazame nguvu zake, alizo nazo kiunoni mwake, nao uwezo wake uliomo mishipani mwa tumbo lake. Hunyosha mkia wake, uwe kama mwangati, mishipa ya mapaja yake imefungamana. Mifupa yake ndio mabomba ya shaba, nazo mbavu zake ndio fimbo za chuma. Wa kwanza wa viumbe vya Mungu ndiye yeye, naye aliyemwumba alimgawia nao upanga wake. Mapori ya milimani humtolea chakula, nao nyama wote wa porini huchezacheza hapo. Hulala chini ya miti yenye kivuli hujificha penye matete mabwawani. Ile miti yenye kivuli humfunika kwa kivuli chao, nayo mifuu ya mtoni humzunguka. Tazama, ijapo maji ya mto yafurike sana, hastuki kamwe, hutulia, ijapo mto kama Yordani umshambulie kuingia kinywani. Yuko nani atakayemkamata, akiwa macho? Au yuko nani atakayeitoboa pua yake, amfunge kwa kamba? Je? Unaweza kumvua nondo wa baharini kwa ndoana au kuufunga ulimi wake kwa kamba katika taya la chini? Au utaweza kumtia ugwe puani mwake? Au utaweza kulitoboa shavu lake kwa kulabu? Je? Atazidi kukulalamikia? Au atakuambia maneno ya upole? Atafanya agano na wewe, umchukue, awe mtumishi wako kale na kale? Je? Utamchezesha kama ndege, ukimfunga wa kufurahisha vijana wa kike? Chama cha wavuvi kinamchuuzia na kuwagawanyia wachuuzi vipande vipande? Je? Utaweza kueneza mikuki ngozini pake au kichwani pake vyusa vya wavuvi? Haya! Mpelekee mkono wako, umkamate! Ndipo, utakapolikumbuka pigano hilo, usilirudie tena. Tazama! Hicho kingojeo cha kumkamata ni uwongo, ukimtazama tu utakufa ganzi. Hakuna ajipaye moyo wa kumwamsha; tena yuko nani atakayesimama usoni pangu, mimi Mungu? Yuko nani aliyeanza kunipa kitu, nimlipe? Yote pia yaliyoko chini ya mbingu ni yangu mimi. Sitanyamaza, nisiseme, jinsi viungo vyake vilivyo, nazo nguvu zake, jinsi zilivyo kubwa, nayo matengenezo yake, jinsi yalivyo mazuri. Yuko nani awezaye kulichuna vazi lake? Yuko nani atiaye mkono katika mataya yake yenye meno mawilimawili? Yuko nani awezaye kuifungua milango ya kinywa chake? Kwani pande zote zinayo meno yaogopeshayo. Magamba yake ni mazuri mno kwa hivyo, yanavyojipanga: kama ni kukazwa kwa nguvu ya chapa, hugandamana karibukaribu, hushikamana kabisa kila moja na mwenzake, upepo tu usiweze kupita katikati yao. Kweli kila moja linagandamana na mwenzake, yanashikana kwa nguvu, yasitengeke. Akienda chafya humulikisha mwanga, nayo macho yake yanafanana nayo makope ya mapambazuko. Mienge ya moto hutoka kinywani mwake, nayo hurukisha macheche ya moto. Katika mianzi ya pua yake hutoka moshi kama wa chungu kichemkacho au wa moto wa matete. Pumzi yake huunguza kama makaa yenye moto, hata miali ya moto hutoka kinywani mwake. Shingoni pake ndipo, nguvu zinapokaa, mbele yake yako matetemeko na mastusho. Manofu ya mwili wake yanashupaa, kwa kukazana hapo, yalipo, hayatikisiki. Moyo wake nao ni mgumu kama jiwe, ugumu wake ni kama wa jiwe la chini la kusagia. Akiinuka, nao wenye nguvu hushikwa na woga, kwa kustushwa hukosa njia ya kukimbilia. Ukimpiga kwa upanga haumwingii, wala mkuki wala mshale wala chuma cho chote. Chuma hukiwazia kuwa jani kavu, nayo shaba huiwazia kuwa mti uliobunguka. Mishale ya upindi haiwezi kumkimbiza, nayo mawe ya kombeo kwake hugeuka kuwa kama makapi. Marungu huwaziwa naye kuwa mabua makavu, tena huicheka shindo ya mkuki, ukitupwa. Upande wake wa chini una vigae vyenye pembe, alipogaagaa ni kama matopeni, palipopita gari la kupuria. Hukichafua nacho kilindi, kiwe kama chungu kinachochemka; huivuruga nayo bahari, iwe kama dawa, zikivurugwa chunguni. Nyuma yake hiyo njia, aliyoishika, huangazika, hilo povu la kilindi mtu angeliwazia kuwa mvi. Huku nchini hakuna afananaye naye; alichoumbiwa, ni hiki: asistuke kamwe! Wote walio wakuu huwatazama tu, kuliko wenye majivuno wote mfalme ndiye yeye. Iyobu akamjibu Bwana akisema: Ya kuwa unayaweza yote, ninayajua; uliyoyataka, hayazuiliki. Yuko nani awezaye kuyatowesha mashauri yako? Maana ni mtu asiyejua kitu. Kweli nimesema, nisiyoyatambua, mastaajabu kama hayo yananishinda, siyajui. Sikiliza, niseme nami! Nitakuuliza, unijulishe! Kusikia naliyasikia mambo yako kwa masikio yangu, lakini sasa macho yangu yamekuona. Kwa hiyo nayatangua mwenyewe, niliyoyasema, humu mavumbini na majivuni ninajuta. Ikawa, Bwana alipokwisha kumwambia Iyobu maneno haya, Bwana akamwambia Elifazi wa Temani: Makali yangu yamekuwakia wewe na wenzako hawa wawili, kwani maneno, mliyoyasema kuwa yangu, hayakunyoka kama yale ya mtumishi wangu Iyobu. Sasa jichukulieni ng'ombe waume saba na kondoo waume saba, mwende kwa mtumishi wangu Iyobu, mwatoe kuwa ng'ombe za tambiko zenu ninyi, naye mtumishi wangu Iyobu na awaombee; kwani kwa kumpendelea yeye nitaacha kuwafanyizia ninyi yaupasayo ujinga wenu, kwani maneno, mliyoyasema kuwa yangu, hayakunyoka kama yale ya mtumishi wangu Iyobu. Ndipo, Elifazi wa Temani na Bildadi wa Sua na Sofari wa Nama walipokwenda, wakafanya, kama Bwana alivyowaambia, naye Bwana akampendelea Iyobu. Kisha Bwana akayafungua mafungo ya Iyobu, alipowaombea wenzake; nayo yote, Iyobu aliyokuwa nayo, Bwana akayarudisha na kuyaongeza, akayapata yale ya kale mara mbili. Wakaja kwake ndugu zake wote wa kiume na wa kike nao waliojuana naye kale, wakala naye chakula nyumbani mwake, wakampongeza na kumtuliza moyo kwa ajili ya hayo mabaya yote, Bwana aliyokuwa alimletea, wakampa kila mtu kipande cha fedha na pete ya dhahabu. Hivyo Bwana akambariki Iyobu, mwisho wake utukuke kuliko mwanzo, akapata kondoo na mbuzi 14000 na ngamia 6000 na majozi 1000 ya ng'ombe na majike ya punda 1000. Akapata tena wana saba wa kiume na watatu wa kike. Hao akawaita majina yao, wa kwanza Yemima (Hua), wa pili Kesia (Marashi), wa tatu Kereni-Hapuki (Pembe ya Wanja). Hawakuonekana wanawake katika nchi yote nzima waliokuwa wazuri kama hao mabinti Iyobu. Naye baba yao akawapa mafungu, yawe yao, kama waumbu zao. Hayo yote yalipokwisha, Iyobu akawapo miaka 140, akaona wana na wajukuu, vizazi vinne. Kisha Iyobu akafa alipokuwa mzee mwenye miaka mingi ya kumtosha. *Mwenye shangwe ni mtu asiyefuata shauri lao wasiomcha Mungu, asiyesimama njiani kwao wakosaji, asiyekaa penye kao la wafyozaji. Ila hupendezwa na Maonyo yake Bwana, hayo Maonyo yake ndiyo, ayawazayo mchana na usiku. Kwa hiyo atakuwa kama mti uliopandwa penye vijito, uzaao matunda yake, siku zinapotimia, nayo majani yake hayanyauki; yote ayafanyayo hufanikiwa. Lakini wasiomcha Mungu sivyo walivyo, wao hufanana na makapi, upepo uyapeperushayo. Kwa hiyo wasiomcha Mungu hawataopolewa kwenye mapatilizo, wala wakosaji kwenye mkutano wao waongofu. Kwani Bwana huijua njia yao walio waongofu, lakini njia yao wasiomcha Mungu itapotea.* Mbona wamizimu hupiga makelele? Mbona makabila ya watu huwaza mambo yaliyo ya bure? Wafalme wa nchi hushikana mioyo, wakuu nao hula njama wakikaa pamoja, wamkatae Bwana na Masiya wake kwamba: Na tuyavunje mafungo yao! na tuzitupe kamba zao, zisitufunge tena! Lakini akaaye mbinguni anawacheka, yeye Bwana anawafyoza. Siku zitakapotimia, atasema nao kwa makali yake, awastushe kwa moto wa machafuko yake: Mimi nimemsimika mfalme wangu huko mlimani kwa Sioni kwenye utukufu wangu. Nitasimulia shauri, Bwana aliloniambia: Wewe ndiwe Mwanangu, siku hii ya leo mimi nimekuzaa. Omba kwangu! Nami nitakupa wamizimu, wawe fungu lako, nayo mapeo ya nchi, yawe mali zako! Kwa fimbo ya chuma utawaponda, kama vyombo vya mfinyanzi utawavunja. Sasa nyie wafalme, pambanukeni! Nanyi waamuzi wa nchi, onyekani! Mtumikieni Bwana kwa kumwogopa! Mshangilieni kwa kutetemeka! Mnoneeni Mwana, asiwatolee makali, mkaangamia njiani! Maana moto wa makali yake utawaka upesi. Wenye shangwe ndio wote wamwegemeao! Bwana, tazama, jinsi walivyo wengi wanaonisonga! Tena ni wengi wanaoniinukia. Ndio wengi wanaoiwazia roho yangu ya kwamba: Hapana wokovu, atakaoupata kwake Mungu. Lakini wewe Bwana, u ngao inikingiayo, kwa kuwa utukufu wangu utakikweza kichwa changu. Ninapoipaza sauti yangu, ifike kwake Bwana, huniitikia toka mlimani kwenye utakatifu wake. Mimi nililala usingizi, kisha nikaamka, kwani mwenye kunishikiza ni Bwana. Ijapo, watu wawe maelfu na maelfu, siwaogopi, wakija kunipangia na kunizunguka. Inuka, Bwana! Niokoe, Mungu wangu! Kwani walio adui zangu unawapiga makofi wote, ukawavunja meno wasiokucha, wewe. Kwako Bwana uko wokovu, uwapatie mema wao walio ukoo wako. Ninapokulilia, niitikie, Mungu unipaye wongofu! Hunipatia mahali pakubwa, nikiwa nimesongwa; sasa nihurumie na kuyasikia maombo yangu! Ninyi wana wa watu mpendao mambo ya bure, mpaka lini mwanitia soni na kuninyima heshima, mpaka lini mtayanyatia yaliyo uwongo tu? Lakini tambueni, ya kuwa Bwana humkuza amchaye! Bwana hunisikia, kila ninapomlilia. Stukeni, msije kukosa! Semeni mioyoni mwenu, mnapolala, mpate kutulia! Tambikeni na kutoa vipaji vya tambiko vyenye wongofu, nanyi mpate kumwegemea aliye Bwana! Wako wengi wanaosema kwamba: Yuko nani atakayetuonyesha kilicho chema? Bwana, utokeze mwanga wa uso wako, uwe juu yetu! Umenipa furaha moyoni mwangu ipitayo yao ya kufurikiwa na vyakula na vinywaji. Hivyo nitalala usingizi na kutengemana pia, kwani wewe ndiwe Bwana peke yako, unanipatia makao yasiyoshindika. Bwana, yasikilize maneno yangu! Yatambue nayo manong'ono yangu! Sauti ya kilio changu itegee masikio! Mfalme wangu na Mungu wangu, ninakulalamikia. Bwana, asubuhi uisikie sauti yangu! Asubuhi ninajiweka kuwa tayari, nikuchungulie. Kwani wewe siwe Mungu apendezwaye naye asiyekucha, wala mtu mbaya hakai huko, uliko. Wajitukuzao hawasimami machoni pako; unawachukia wote wafanyao maovu. Utawaangamiza kabisa wao wasemao uwongo, wenye kiu ya damu na wadanganyaji humtapisha Bwana. Lakini mimi kwa wingi wa upole wako nitaingia Nyumbani mwako, nikuangukie Patakatifu pako pa kuombea, kwa maana ninakuogopa. Bwana, niongoze, niufuate wongofu wako, kwa ajili yao waninyatiao, ukainyoshe njia yako machoni pangu! Kwani vinywani mwao hao hamna yaliyo sawa, mioyoni mwao hukaa tamaa mbaya tu, makoo yao huwa makaburi yaliyo wazi, ndimi zao nazo huteleza. Wapatilize, Mungu, waangushwe na mashauri yao, wakumbe kwa ajili ya maovu yao mengi! Kwani wamekubisha. Wote wakuegemeao wapate kufurahi kale na kale, wapige vigelegele, kwani huwakingia, wakushangilie wote walipendao Jina lako! Kwani wewe, Bwana, unambariki aliye mwongofu, ukamvika upendelevu, kama ni ngao. Bwana usinipatilize kwa makali yako, wala kwa machafuko yako yenye moto usinichape! Bwana, na uniwie mpole, kwani ni mnyonge; kwa kuwa mifupa yangu imestuka, niponye Bwana! Nayo roho yangu imestuka sana, nawe Bwana, utakawia mpaka lini? Ee Bwana, rudi, uiopoe roho yangu! Niponye kwa hivyo, ulivyo mwenye utu! Kwani kwao waliokwisha kufa hakuna anayekukumbuka, nako kuzimuni yuko nani atakayekushukuru? Kwa kupiga kite nimechoka, nikakiogesha kitanda changu usiku wote, nikayalowesha malalo yangu kwa machozi yangu. Macho yangu yamenyauka kwa uchungu, yakachakaa kwa ajili yao wote wanisongao. Ondokeni kwangu, nyote mfanyao maovu! Kwani Bwana huzisikia sauti za kilio changu. Bwana husikia, ninavyomlalamikia, Bwana huyapokea maombo yangu. Adui zangu watapatwa na soni wote kwa kustushwa sana, watarudi nyuma kwa kuingiwa na soni kwa mara moja. Bwana Mungu wangu, nimekukimbilia wewe. Nisaidie, uniokoe mikononi mwao wote wanikimbizao! Wasiirarue roho yangu kama simba, wakainyafuanyafua, nisipopata mwokozi! Bwana Mungu wangu, kama yako mambo, niliyoyafanya, kikawamo kipotovu mikononi mwangu, kama nimemkorofisha mwenzangu, tuliyepatana naye, naye aliyenisonga bure nikamwokoa: basi, mchukivu na aikimbize roho yangu, aikamate na kunikanyaga hapo chini, anitoe uzimani, nao utukufu wangu aukalishe mavumbini! Inuka, Bwana, kwa makali yako! Jikweze, ukinge moto wa makorofi yao wanisongao! Amka, uje kwangu wewe uliyeagiza kuhukumu. Mkutano wa makabila ya watu sharti ukuzunguke, kisha hapo, walipo, urudi kuwa juu yao! Bwana ndiye atakayewahukumu watu wote; nami niamulie, Bwana, kwa kuwa mwongofu pasipo kosa, nifanyalo. Ubaya wao wasiomcha Mungu sharti ukomeshwe, lakini mwongofu umshikize, apate kusimama! Mwenye kujaribu mioyo na mafigo ni wewe, Mungu mwongofu. Ngao yangu iko kwake Mungu, naye huwaokoa wao wanyokao mioyo. Mungu ni mwamuzi mwenye wongofu, ni Mungu atishaye kila siku: mtu akikataa kugeuka, ataunoa upanga wake, nao uta wake ataupinda na kuuelekeza. Vyombo viuavyo ndivyo, atakavyopachika humo, nayo mishale yake ataiwakisha moto. Mwenye kujifunga, atokeze kiovu, mtazameni: huwa kama mwenye mimba ya kuzaa maumivu, lakini anapozaa, ni madanganyo ya kumdanganya yeye! Akiwa amechimba shimo na kulitanua, hutumbukia mwenyewe mlemle mwenye mwina, alioutengeneza yeye. Maumivu yake ya kuumiza wengine humrudia kichwani pake, nayo makorofi yake humshukia utosini. Kwa ajili ya wongofu wake namshukuru Bwana, naliimbia Jina lake Bwana Alioko huko juu. Bwana Mungu wetu, Jina lako hutukuka sana katika nchi zote, maana umeutanda utukufu wako kule mbinguni. Vinywani mwao watoto wachanga namo mwao wanyonyao ulijitengenezea tukuzo, upate kuwashinda wao wakupingiao, upate kumnyamazisha hata mchukivu naye ajilipizaye. Ninapozitazama mbingu zako, vidole vyako vilizoziumba, hata mwezi nazo nyota, ulizoziweka wewe, basi, mtu ndio nini, umkumbuke? mwana wa mtu naye, umkague? Ulimpunguza kidogo, asilingane na wewe, Mungu, lakini macheo na mapambo yenye utukufu ndiyo, uliyomvika. Ukampa kuyatawala yote, mikono yako iliyoyafanya, yote pia ukayaweka kuwa chini miguuni pake: kondoo na ng'ombe wote pamoja, nao nyama wa porini, hata ndege wa anga nao samaki wa baharini, nao nyama wote waliomo vilindini mwa bahari. Bwana Mungu wetu, Jina lako hutukuka sana katika nchi zote. Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote, nitayasimulia mataajabu yako, uliyoyafanya yote. Kwa kufurahi nitakushangilia, nitaliimbia Jina lako wewe ulioko huko juu, kwani adui zangu wamerudi nyuma, wakajikwaa, wakaangamia machoni pako. Maana umenipatia kushinda, nilipohukumiwa, ukakalia kiti cha uamuzi, utoe hukumu iongokayo. Umekaripia wamizimu, ukaangamiza wasiokucha, ukayafuta majina yao, yasiwepo tena kale na kale. Adui wamemalizika, nako walikokaa kutakuwa na maheme tu kale na kale, maana miji yao umeibomoa, kumbuko lao likaangamia. Bwana hukaa kale na kale, akakisimika kiti chake, atoe hukumu. Yeye ndiye atakayeuhukumu ulimwengu kwa wongofu, ayaamue makabila ya watu kwa unyofu. Hivyo Bwana ni ngome yao waliokorofika, katika siku za masongano ni ngome kweli. Walijuao Jina lako watakuegemea, kwani wanaokutafuta, Bwana, huwaachi. Mshangilieni Bwana akaaye Sioni! Tangazeni matendo yake kwenye makabila ya watu! Kwa kuwa ni mwenye kulipiza damu, huwakumbuka, malalamiko yao wakiwa hayasahau. Nihurumie, Bwana, ukitazama, ninavyoteswa nao wanaonichukia! Maana aliyenikweza na kunitoa malangoni mwa kufa ni wewe. Hivyo nitayasimulia matukuzo yako yote malangoni mwa binti Sioni na kupiga vigelegele, kwa sababu umeniokoa. Wamizimu wamedidimia katika shimo, walilolifanya wao, miguu yao ikanaswa katika tanzi, walilolitega wenyewe. Hivyo Bwana hujulika anapofanya hukumu, huwanasa kwa kazi za mikono yao wao wasiomcha. Wasiomcha Mungu watarudi kuzimuni, nao wamizimu wote pamoja nao wanaomsahau Mungu. Kwani mkiwa hasahauliwi kale na kale, wala kingojeo chao wanyonge hakiangamii zamani zote. Inuka, Bwana, watu wasikaze nguvu, wamizimu wahukumiwe machoni pako! Wakemee wamizimu, Bwana, kusudi wastushwe, kusudi wajitambue kuwa watu tu! Bwana, ukisimama mbali, ni kwa sababu gani? Ukaja kujificha siku za kusongeka? Kwa majivuno yao wasiokucha mnyonge hutishika, na watekwe kwa mapotovu, waliyoyawaza! Asiyemcha Mungu hujivunia tamaa za roho yake, naye mwenye choyo humtukana Bwana na kumbeza. Asiyemcha Mungu huvimba kichwa kwamba: Halipishi; mawazo yake yote ni kwamba: Hakuna Mungu. Njia zake huendelea kwa nguvu siku zote, kwani mapatilizo yako humkalia mbali, wote wamsongao huwafokea. Husema moyoni mwake: Sitatikisika, vizazi na vizazi vitapita, nisipatwe na kibaya. Kinywa chake hujaa viapizo na mapunjo ya kudanganya watu, nayo makorofi na maovu yamo chini ya ulimi wake. Hukaa nyuani na kuotea, amwue asiyekosa, watu wasipovijua, macho yake hutunduia walio wanyonge. Hunyata na kujifichaficha kama simba kichakani, humnyatia mnyonge, amkamate, humkamata mnyonge kweli na kumnasa tanzini. Maana huwatambalia na kunyemelea, mpaka wao wakiwa waanguke makuchani mwake. Husema moyoni mwake: Mungu amewasahau, ameuficha uso wake, asiwatazame kale na kale. Inuka, Bwana! Nao mkono wako uunyoshe, Mungu! Usiwasahau hao walio wanyonge! Sababu gani wakubeze, Mungu, wao wasiokucha wakisema mioyoni mwao: Hutalipisha? Kwa kuyatazama makorofi na maumivu umeyaona hayo, namo mkononi mwako ndimo, yalimo sasa; akorofikaye hukuachilia wewe mambo yake yote, naye aliyefiwa na wazazi, wewe humwia msaidiaji. Ivunje mikono yake asiyekucha kwa kuwa mbaya! Yalipize mabezo yake, yasionekane tena! Bwana ni mfalme siku zote zitakazokuwa kale na kale, wamizimu sharti waangamie nchini kwake. Wanyonge umewasikia, Bwana, walipokupigia kite, ukaishikiza mioyo yao na kuwasikiliza kwa masikio yako. Huwaamulia waliofiwa na wazazi, nao wakorofikao, mtu asifulize tena kujivuna huku nchini. Bwana ndiye, nimkimbiliaye, nanyi mnaiambiaje roho yangu: Rukia mlimani kama ndege? Kwani watazameni wasiomcha Mungu, wanapinda pindi, wakapachika mishale penye upote, wapige gizani wanyokao mioyo. Misingi inapobomolewa, mwongofu atafanyaje? Bwana yumo Jumbani mwake mwenye utakatifu, yeye Bwana kiti chake cha uamuzi kiko mbinguni, macho yake huwachungulia wana wa watu, kope zake ziwajaribu. Bwana humjaribu naye mwongofu, roho yake humchukia asiyemcha naye apendaye ukorofi. Atawanyeshea matanzi wao wasiomcha, tena mvua za moto na za viberitiberiti, nao upepo wa kuchoma moto ndio kinywaji, watakachogawiwa. Kwani Bwana ni mwongofu, hupenda yaongokayo; kwa hiyo anyokaye moyo atauona uso wake. Okoa, Bwana! Kwani wamekwisha wao wakuchao, nao wakutegemeao wametoweka kwenye wana wa watu. Kila mtu na mwenzake husemeana yaliyo uwongo, midomo yao husema yenye ujanja, kwa kuwa wenye mioyo miwili. Bwana na akomeshe midomo yote yaliyo yenye ujanja, nazo ndimi zisemazo maneno makuu tu! Ndio wanaosema: kwa nguvu za ndimi zetu tutashinda sisi, nayo mikono yetu hutusaidia; yuko nani atakayetutawala? Kwa ajili ya taabu zao walio wanyonge na kwa ajili ya yowe zao walio wakiwa nitainuka sasa, ndivyo, Bwana asemavyo, niwapatie wokovu wauchuchumiao. Maneno ya Bwana ndiyo maneno yaliyo mang'avu hufanana na fedha zilizoyeyushwa chunguni huku nchini, zilizong'azwa hivyo mara saba. Wewe, Bwana, utayaangalia! Nasi utatuokoa katika uzazi huo kale na kale! Wasiokucha huendelea na kutuzunguka, kwani maoneo ndiyo yanayotukuzwa kwao watu. Mpaka lini, Bwana, utanisahau kila mara? Mpaka lini utauficha uso wako, usinione? Mpaka lini nitie wasiwasi rohoni mwangu na masikitiko moyoni mwangu kila siku? Mpaka lini ataniinukia mchukivu wangu? Nitazame, ukaniitikie, Bwana Mungu wangu! Yaangaze macho yangu, nisipatwe na usingizi uuao! Mchukivu wangu asiseme: Nimemshinda! Nao wanisongao wasishangilie, ya kuwa nimetikisika! Nami nimeuegemea upole wako; moyo wangu hushangilia, ya kuwa unaniokoa; nitamwimbia Bwana kwa ajili ya mema, aliyonitendea. Mpumbavu husema moyoni mwake: Hakuna Mungu. Hawafai kitu, mapotovu yao hutapisha, anayefanya mema hayuko. Bwana huchungulia toka mbinguni awatazame wana wa watu, aone, kama yuko mwenye akili anayemtafuta Mungu. Wote pamoja wamepotelewa na njia, wote ni waovu, hakuna anayefanya mema; hakuna hata mmoja. Je? Wale wote wafanyao maovu hawataki kujitambua, wao wanaowala walio ukoo wangu, kama walavyo mkate? Lakini Bwana hawamtambikii! Patafika, watakapotetemeka kwa kustuka, kwani Mungu yuko kwao walio wazao waongokao. Shauri la mnyonge mnalibezesha, kwa maana Bwana ndiye, anayemjetea. Laiti mwokozi wake Isiraeli atokee Sioni, Bwana awarudhishe mateka walio wa ukoo wake! Ndipo, Yakobo atakaposhangilia, ndipo, Isiraeli atakapofurahi. Bwana, yuko nani atakayetua hemani mwako? Yuko nani atakayekaa mlimani kwenye utukufu wako? Ni yeye ayendeleaye yaliyo sawa na kufanya yaongokayo, ni yeye awazaye moyoni mwake yaliyo kweli. Ulimi wake hausemi yaliyo masingizio; hamfanyizii mwenziwe kibaya, naye, waliyetua pamoja, hamtii soni. Aliyetupwa si kitu machoni pake, lakini wamchao Bwana anawaheshimu; kama ameapa, hageuzi, ijapo yampatie mabaya. Mali zake hazikopeshi, zimpatie faida nyingi, wala hatwai mapenyezo ya kumpatiliza asiyekosa. Aendeleaye hivyo hatatikisika kale na kale. Unilinde, Mungu! Kwani nimekukimbilia. Nimemwambia Bwana: Wewe u bwana wangu; hakuna nionacho kuwa chema kisichotoka kwako. Nao watakatifu waliopo katika nchi nimewaambia: Hawa ndio wakuu wa kweli, ndio wanipendezao kabisa. Maumivu yao wakimbiliao mwingine yatakuwa mengi; sitavimimina vinywaji vyao vya tambiko, maana ni vyenye damu, wala majina yao sitayatia tena midomoni mwangu. Bwana ni fungu langu, nililolitwaa, tena ni kinyweo, nilichopewa; wewe unanishikizia niliyopatiwa nilipopigiwa kura; kamba zake ziliponiangukia niligawiwa pazuri, hilo fungu, nililolitwaa, linapendezeka kweli. Nitamkuza Bwana aniongozaye, mafigo yangu hunionya hivyo hata usiku. *Bwana na anisimamie kila, nitakapokuwa, awe kuumeni kwangu, nisitikisike. Kwa hiyo moyo wangu hufurahi, nayo yaliyo utukufu wangu hushangilia, hata mwili wangu utatulia kwa kuwa na kingojeo. Kwani hutaiacha roho yangu, ipotee kuzimuni, wala hutamtoa akuchaye, apate kuoza kaburini. Unanitambulisha njia iendayo penye uzima, utanishibisha furaha zilizopo usoni pako; mkono wako wa kuume hutoa kale na kale yapendezayo.* E Bwana, sikia jambo liongokalo! Yaitikie malalamiko yangu! Sikiliza nikuombayo na midomo isiyodanganya! Wewe uniamulie shauri langu, maana macho yako huyatazama yaliyonyoka. Umeujaribu moyo wangu na kunikagua usiku, ukaning'aza motoni pasipo kuona kibaya; nikajikaza moyoni kwa ajili ya kinywa changu, kisipite mpaka. Matendo ya mtu yalivyo, ndivyo, midomo yake iumbuavyo; mimi nimejiangalia, nisizifuate njia zao walio wakorofi. Miguu yangu hushika sawasawa, uiongozapo, nazo nyayo zangu hazikutangatanga. Mimi nikakuita, Mungu, kwani huniitikia; unitegee sikio lako, usikie ninayokuambia! Toa magawio yako yastaajabishayo! Kwani huwaokoa wakujeteao, kwa nguvu ya mkono wako huwatoa mikononi mwao wawainukiao. Nilinde na kuniangalia kama mboni ya jichoni! Nifiche kivulini mwa mabawa yako! Nisiwaonekee waovu wanikorofishao, wala wachukivu wangu waizungukao roho yangu! Mioyo yao migumu huishupaza, navyo vinywa vyao husema majivuno. Tukiwa tunajiendea tu, mara hutuzuia wakitumbuliza macho, wapate kutuangusha chini. Hufanana na simba atamaniye kunyafua, au na mwana wa simba anyatiaye na kujifichaficha. Inuka, e Bwana! Umjie mbele, upate kumbwaga! Kwa upanga wako iokoe roho yangu mikononi mwake asiyekucha! Mkono wako, Bwana, uniokoe mikononi mwa waume, ambao kiume chao ni cha dunia hii, fungu lao nalo liko nchini tu. Matumbo yao uyajaze mali zako, washibe pamoja na wana wao, tena watakazozisaza waziachie hao watoto wao! Lakini mimi kwa hivyo, nilivyo mwongofu, nautazamia uso wako, niamkiapo nipate kushiba kwa kukuona, ulivyo wewe. Akasema Nakupenda kwa moyo, Bwana, uliye nguvu yangu. Bwana ni ngome yangu na boma langu, tena ni mponya wangu, ni Mungu aliye mwamba wangu, kwa hiyo ninamjetea; ni ngao yangu na pembe ya kunipatia wokovu, tena ni kingo langu. Bwana atukuzwaye ndiye, ninayemwitia; ndipo, ninapookolewa mikononi mwao walio adui zangu. Kamba ziuazo zilikuwa zimeniasamia, nayo majito yaangamizayo yalinistusha; kamba zivutiazo kuzimuni zilikuwa zimenizunguka, nayo mafungo yauayo yalikuwa mbele yangu. Hapo niliposongeka nalimwita Bwana, yeye aliye Mungu wangu nikamlalamikia, akaisikia sauti yangu Jumbani mwake, malalamiko yangu ya usoni pake yakamwingia masikioni mwake. Nchi ikatukutika na kutetemeka, nayo misingi ya milima ikatikisika kwa kutukuswa, kwani aliitolea makali yake yenye moto. Moshi ukapanda puani mwake, moto ulao ukatoka, kinywani mwake, makaa ya moto yakamulikamulika mbele yake. Akatanda mbingu ya kushukiapo, mawingu meusi yakawa chini ya miguu yake. Akapanda gari, nalo likarushwa, likakimbizwa mbiombio mabawani mwa upepo. Akatumia giza kuwa ficho lake, limfunike pande zote likiwa kao lake; ndio mawingu meusi yenye mvua kali. Kwa nguvu ya kumulika mbele yake mawingu yakatutumka, mvua ya mawe ikanyesha pamoja na kupiga umeme. Bwana akapiga ngurumo kule mbinguni, Alioko huko juu akaivumisha sauti yake, mvua ya mawe ikanyesha pamoja na kupiga umeme. Alipoipiga mishale yake, akawatawanya, ngurumo zilipozidi kuwa nyingi, wakapigwa bumbuazi. Ndipo, ilipoonekana mikondo ya maji, nayo misingi ya nchi ikafunuliwa kwa nguvu ya makaripio ya kwako, Bwana, na kwa ukali wa pumzi ya pua yako. Akakunjua mkono toka juu, akanikamata, mle mlimo na maji mengi akanichopoa. Akaniponya mikononi mwa adui yangu mwenye nguvu, namo mwao walionichukia kwa kuwa na uwezo kuliko mimi. Walikuwa wamenijia mbele ile siku, nilipokuwa nimeshindwa, lakini Bwana akanijia kuwa shikizo. Akanitoa kwao, akanikalisha palipo papana; ndivyo, alivyoniopoa kwa kupendezwa nami. Yaupasayo wongofu wangu Bwana alinipa, akanipatia tena yaupasayo ung'avu wa mikono yangu. Kwani naliziangalia njia zake Bwana, nisifanye kilicho kiovu mbele yake Mungu wangu. Kwani maamuzi yake yote yako mbele yangu, nayo maongozi yake sikuyaacha, nisiyafuate. Nikawa naye pasipo kuonywa, nikajiangalia, nisimkosee. Bwana akanipatia tena yaupasayo wongofu wangu, kwa kuwa mikono yangu ilikuwa imeng'aa machoni pake. Wewe humwia mpole aliye mpole, naye aliye mkweli wote nawe humwia mkweli wote. Wewe humwia mng'avu aliye mng'avu, lakini aliye mpotovu nawe humpotokea. Kwani walio wanyonge wewe huwaokoa, lakini macho yajivunayo huyanyenyekeza. Kwani wewe ndiye anayeiwasha taa yangu, wewe Bwana, Mungu wangu, huliangaza nalo giza langu. Kwani nitashambulia vikosi vizima kwa nguvu yako, kwa nguvu ya Mungu wangu narukia napo ukutani. Njia yake Mungu haipindiki, Neno lake Bwana limeng'azwa. Yeye ni ngao yao wote wamkimbiliao. Kwani yuko nani aliye Mungu, asipokuwa Bwana? Tena yuko nani aliye mwamba, asipokuwa Mungu wetu? Ni yeye Mungu aliyenivika nguvu, njia yangu huitengeneza, iwe imenyoka kabisa. Hunipatia miguu ikimbiayo kama ya kulungu, anisimamishe kwangu vilimani juu. Huifundisha mikono yangu kupiga vita, mpaka mikono yangu iweze kupinda hata uta wa shaba. Hunipa ngao ya kuniokoa, kuumeni kwako hunishikiza, napo hapo, unaponinyenyekeza, hunikuza. Huipanulia miguu yangu, ipate pa kupitia, viwiko vyangu vya miguu visiteleze. Nitawakimbiza adui zangu, mpaka niwakamate; sitarudi, nisipokwisha kuwamaliza. Nitawaponda, wasiweze kuinuka tena. Sharti waanguke miguuni pangu. Hunivika nguvu ya kupiga vita, huwalaza chini yangu wao waniinukiao. Hunipa adui zangu, niwaone migongo, nipate kuwanyamazisha wachukivu wangu. Hakuna mwokozi, wanapolalamika, wanapomwitia Bwana, hawaitikii. Nitawaponda, mpaka wabunguke kama mavumbi upeponi, niwazoe kama mataka yaliyoko viwanjani. Kwenye magomvi ya watu ulinitoa, ukanipa kuwa kichwa chao wao wamizimu, watu, ambao nilikuwa siwajui, wanitumikie. Masikio yao yanaponisikia, hunitii, nao watokao mbali hunipongeza. Hao watokao mbali walikuwa wamenyauka, walipotoka mabomani kwao na kutetemeka. Bwana Mwenye uzima ni mwamba wangu upasao kusifiwa, yeye Mungu aliyeniokoa sharti atukuke! Mungu ndiye aliyenipatia malipizi na kuteka makabila ya watu, wanitii. Wewe ndiwe uliyeniokoa mikononi mwao walio adui zangu, kwao waniinukiao ukaniweka kuwa mkuu wao, kwao walionikorofisha ukaniponya. Kwa hiyo nitakushukuru, Bwana, kwenye wamizimu, nalo Jina lako na niliimbie. Mfalme wake alimpatia wokovu mwingi, aliyempaka mafuta humfanyizia yenye upole; huyo ni Dawidi naye aliye wa uzao wake kale na kale. Mbingu zinausimulia utukufu wake Mungu, yaliyoko juu huyatangaza matendo ya mikono yake. Siku huambia siku mwenziwe utume huo, nao usiku huutambulisha usiku mwenziwe. Hakuna msemo wala maneno, sauti zao zisisikilike mumo humo. Uvumi wao ulitokea katika nchi zote, nayo maneno yao yalifika hata mapeoni kwa ulimwengu; hata jua alilionea kituo hukohuko. Nalo hutokea, kama mchumba anavyotoka chumbani mwake, hufurahia kupiga mbio njiani kama mpiga vita. Kwenye mwisho wa mbingu ndiko, linakokucha, huendelea, mpaka lichwe kwenye mwisho wake mwingine, hakuna panapojificha, lisipawakie. Maonyo yake Bwana yanayo kweli yote, hutuliza roho; ushahidi wake Bwana hutegemeka, hupambanusha wapumbavu. Maagizo yake Bwana hunyoka, hufurahisha mioyo, amri zake Bwana hung'aa, huangaza macho. Kumwogopa Bwana hutakasa, kutakuwapo kale na kale; maamuzi yake Bwana ni ya kweli, yote pamoja yameongoka. Hayo hutunukiwa kuliko dhahabu, hupita hata dhahabu nyingi zilizong'azwa; tena ni matamu kuliko asali, hupita nao ute wa masega yenye asali. Kisha mtumwa wako huonywa nayo, kuyashika huleta mapato mengi. Yuko nani ajuaye po pote, alipopotelewa? Uning'aze, yaniondokee nayo makosa yajifichayo! Nako kwao wanaokusahau umtoweshe mtumwa wako, wasinitawale! Ndivyo, nitakavyokuwa pasipo kosa, nipate kutakata, yakiniondokea maovu, yaliyokuwa mengi. Maneno ya kinywa changu sharti yakupendeze, nayo mawazo ya moyo wangu sharti yawe wazi mbele yako, Bwana, wewe ndiwe mwamba wangu na mkombozi wangu. Bwana na akuitikie siku ya kusongeka, nalo Jina la Mungu wa Yakobo likuwie ngome! Na atume kwako msaidiaji atokaye Patakatifu pake! Namo Siyoni atokee atakayekushikiza! Na avikumbuke vipaji vyako vyote, ulivyovitoa vya tambiko! Nazo ng'ombe zako za tambiko, ulizomchomea, zimpendeze! Moyo wako uyatakayo na akupe, nayo mashauri yako yote akutimizie! Na tushangilie hivyo, anavyokuokoa! Katika Jina la Mungu wetu na tutweke bendera, Bwana atakapokutimilizia yote, uliyomwomba. Sasa nimejua, ya kuwa Bwana humwokoa, aliyempaka mafuta; akamwitikia mbinguni palipo Patakatifu pake, akamtolea nguvu za kuumeni kwake ziokoazo. Wengine nguvu zao ni magari, nao wengine farasi, lakini sisi tunajikumbusha Jina la Mungu wetu. Hao wakajikwaa, wakaanguka; lakini sisi tukainuka, tukajisimamisha wima. Bwana, tunakuomba, mwokoe mfalme! Nasi siku, tutakapokuita, utuitikie! Bwana, mfalme huifurahia nguvu yako, tazama, jinsi anavyoushangilia mno wokovu wako! Moyo wake uyatunukiayo umempa; wala hukumnyima midomo yake iliyoyaomba. Kwani umemjia na kumletea magawio mema, nacho kichwa chake umekivika kilemba kilicho dhahabu tupu. Alipokuomba uzima, umempa kuwapo, siku zake ziwe nyingi kale na kale. Utukufu, aupatao, ni mkubwa kwa hivyo, unavyomsaidia, hata marembo na mapambo umempatia. Maana umemweka kuwa mbaraka kale na kale, ukamchangamsha, aone furaha iliyo mbele yako. Kwani mfalme amwegemeaye Bwana, hatatikisika kwa upoke wake Alioko huko juu. Mkono wako utawapata adui zako wote, kuumeni kwako kutawapata nao wachukivu wako. Utawafanya kuwa kama jiko la moto, utakapowatokea, Bwana atawameza kwa makali yake, nao moto utawala. Vizazi vyao utaviangamiza, viishie nchini, nazo koo zao sharti zitoweke kwenye wana wa watu. Kwani wamekutegea vibaya, wakakuwazia yenye ujanja, lakini hawakuweza kuyafanyiza. Kwani utawashurutisha kuonyesha migongo, wakikimbia, maana nyugwe za pindi zako utazivuta machoni pao. Tukuka, Bwana, kwa nguvu zako! Nasi tuimbe na kuyakuza matendo ya uwezo wako! *Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Wokovu wangu uko mbali, kwa hiyo napiga kite. Mungu wangu, mchana kutwa nakuita, nawe hikuniitikia; usiku nao hapana, ninaponyamaza. Nawe ndiwe uliye mtakatifu, unakaa na kukuzwa nao Waisiraeli. Wewe nidwe, waliyekutegemea baba zetu, napo walipokutegemea, ukawaopoa. Wewe ndiwe, waliyekulalamikia, wakaponywa, wewe ndiwe, waliyekutegemea, tena hawakupatwa na soni. Lakini mimi ni kidudu, si mtu bado, watu wakanifyoza wote na kunibeza. Wote wanionao hunibeua, hukuza vinywa na kutingisha vichwa, kisha husema: Umsukumie Bwana! Na amponye! Kama anapendezwa naye, na amwokoe! Kwani ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama, ukaniegemeza maziwa yake mama yangu. Wewe ndiwe, niliyetupiwa tangu hapo, nilipozaliwa; tangu hapo, nilipotoka tumboni mwa mama, wewe u Mungu wangu, Kwa kuwa masongano yako karibu, usinikalie mbali! Kwani atakayenisaidia hayuko. Ng'ombe waume wengi wamenizunguka, nao nyati wa Basani wakanizingazinga. Wakaasama vinywa vyao, wanimeze, wakawa kama simba anyafuaye na kunguruma. Nafanana na maji yamwagwayo, mifupa yangu imeteguka yote, moyo wangu ni kama nta iyeyukayo humu mwangu ndani. Nguvu yangu imekupwa, nikavunjika kama gae, nao ulimi wangu umegandamana na ufizi wangu, namo uvumbini mwa kufa ndimo, ulimonilaza. Kwani walikuwako mbwa, wakanizunguka, kikosi cha wabaya kikanijia pande zote, kisha wakanitoboa maganja na nyayo. Naweza kuihesabu mifupa yangu yote, nao wanavitazama tu na kunitumbulia macho. Wakajigawanyia nguo zangu, nalo vazi langu zuri wakalipigia kura. Nawe, Bwana, usiwe mbali! Kwa hivyo, unavyonishupaza, piga mbio, unisaidie!* Iopoe roho yangu kwenye panga! Hiyo iliyo mali yangu peke yake iopoe kwenye mbwa! Namo kinywani mwa simba niokoe, kwani nilipokuwa penye pembe za nyati, uliniitikia. Nitawasimulia ndugu zangu mambo ya Jina lako, nitakuimbia wewe katikati yao walio wateule. Ninyi mmwogopao Bwana, mkuzeni! Vizazi vyote vya Yakobo na vimtukuze! Vizazi vyote vya Isiraeli na vimwangukie! Kwani hakuubeza unyonge wake mnyonge, wala moyo wake hakuuchafukia, wala hakuuficha uso wake, asimwone, ila alimsikia, alipomlilia. Wewe nidwe, nitakayekukuza, makundi mengi yakusanyikapo; nayo niliyomwagia nitayalipa mbele yao wamwogopao. Wanyonge sharti wale, hata washibe; sharti wamshangilie Bwana, wao wamtafutao, mioyo yenu sharti iwepo kale na kale. Hivyo watavikumbuka na kumrudia Bwana mapeoni pote pa nchi; yatakutambikia na kukuangukia makabila yote ya wamizimu. Kwani ufalme ni wake, yeye Bwana, anayewatawala wamizimu ndiye yeye. Wote walio wanene wa nchi watakula na kumwangukia, wote washukao uvumbini huinamia nchi mbele yake yeye, wasioweza kujipauzima ndio wao. Vizazi vyao navyo vitamtumikia Bwana, mambo ya Bwana yatasimuliwa kwao vijukuu. Watakuja, wautangaze wongofu wake kwao watakaozaliwa, kwamba: Ndiye aliyevifanya! *Bwana ni mchungaji wangu, hakuna nitakachokikosa. Hunipumzisha mawandani penye majani mazuri, hunipeleka nako kwenye vijito, nipate kutua. Huutuliza moyo wangu kwa kuniongoza, nifuate mapito yaongokayo, Jina lake litukuzwe. Hata nitakapopita bondeni kwenye giza la kufa, siogopi kibaya, kwani huko nako wewe uko pamoja nami, fimbo yako na mkongojo wako utanishikiza. Wanitandikia meza machoni pao wanisongao, ukanipaka mafuta kichwani pangu, nacho kikombe changu hukijaza, mpaka kimwagikie. Kweli wema na upole utanifuata siku zote za kuwapo kwangu, nikae Nyumbani mwa Bwana siku zitakazokuwa zote.* Nchi hii ni yake Bwana navyo vyote vilivyomo, hata ulimwengu pamoja nao wakaao humu. Kwani yeye aliushikiza kule baharini, nako kwenye majito akaushupaza. Yuko nani atakayepanda mlimani kwa Bwana? Tena yuko nani atakayesimama mahali pake patakatifu? Ni mwenye viganja vitakatavyo naye mwenye moyo ung'aao; ndiye asiyejitia katika mambo ya bure, wala hakuapa uwongo. Mema, Bwana aliyompatia, atayatwaa, ndio wongofu upatikanao kwake Mungu aliye na wokovu wake. Ukoo wao wamtafutao ndivyo, ulivyo, maana hukunyatia wewe, Mungu wa Yakobo, mpaka wauone uso wako. Yanyosheni malango, yawe marefu! Navyo vilango vya kale vipanueni, mfalme mwenye utukufu apate kuingia! Huyu mfalme mwenye utukufu ndiye nani? Ni Bwana Mwenye nguvu, aliye mshindaji, kweli, Bwana ni mshindaji, hushinda vitani. Yanyosheni malango, yawe marefu! Navyo vilango vya kale vipanueni, mfalme mwenye utukufu apate kuingia! Huyu mfalme mwenye utukufu ndiye nani? Bwana Mwenye vikosi, yeye ndiye mfalme, mwenye utukufu. Naikweza roho yangu, ikuelekee Bwana. Mungu wangu, nimekutegemea, sitapatwa na soni, adui zangu wasipate kushangilia kwa ajili yangu mimi. Hawatapatwa na soni kabisa wote wakungojeao, watakaopatwa na soni ndio wakupingao bure. Unijulishe njia zako, wewe Bwana, nayo mapito yake unifundishe! Niendeshe, niyafuate mambo yako ya kweli, ukinifundisha, kwani wewe nidwe Mungu aniokoaye. Wewe ndiwe, nikungojeaye siku zote. Kumbuka, Bwana, huruma zako na magawio ya upoke wako! Kwani yaliyo ya kale na kale ndiyo hayo. Usiyakumbuke maovu, niliyokukosea nilipokuwa kijana, ila unikumbuke kwa upole wako, Bwana, kwani u mwema. Bwana ni mwema na mwongofu; kwa hiyo huonya wakosaji, wakiwa njiani bado. Huongoza wanyonge, wakiamuliwa, kweli hufundisha wanyonge njia yake. Penya upole na kweli ndipo pote, Bwana anapotangulia, kwao walishikao Agano lake nayo mashuhuda yake. Kwa ajili ya Jina lako, Bwana, niondolee manza, kwani hizo, nilizozikora, ni nyingi mno. Mtu amwogopaye Bwana yuko nani? Ndiye, atakayemfundisha njia ifaayo, aichague. Roho yake yeye itakaa palipo pema, nao walio uzao wake wataitwaa nchi. Bwana huwawia mwenzao wa njama wao wamwogopao, nalo Agano lake ndilo, analowajulisha. Macho yangu humtazamia Bwana mchana kutwa, kwani yeye ndiye anasuaye miguu yangu, ikiwa tanzini. Nigeukie, unihurumie! Kwani mimi niko peke yangu na ukiwa wangu. Moyo wangu unaposongeka, uupanulie, kisha unitoe, nilipobanwa! Utazame unyonge wangu na usumbufu wangu, uniondolee yote, niliyoyakosa! Watazame adui zangu! Kwani ni wengi, wakanichukia kwa ukorofi wao uchukizao. Uilinde roho yangu, uniponye! Sitapatwa na soni, kwani nimekukimbilia. Ung'avu na unyofu sharti unikinge, kwani kingojeo changu ndiwe wewe. Mungu, mkomboe Isiraeli katika masongano yake yote! Kwa kuwa mimi nimeendelea pasipo kosa, niamulie, Bwana! Bwana ndiye, nimwegemeaye pasipo kutikisika. Nijaribu, Bwana, na kunipima, unichuje mafigo, hata moyo! Kwani wema wako uko machoni pangu, nami huendelea kukuwia mwelekevu. Sikai pamoja na watu walio wapuzi tu, wala walio wenye kinyume siingii mwao. Ninachukizwa na mkutano wao wafanyao mabaya, wala sikai pamoja nao wambezao Mungu. Nitainawa mikono yangu kwa maji yaondoayo makosa, kisha nitatokea kuzunguka mezani pako, Bwana; ndipo, nitakapozipaza sauti, nikushukuru nikiyasimulia makuu yako yote ya kustaajabu. Bwana, napapenda hapo, Nyumba yako ilipo, ndipo mahali, unapokaa utukufu wako. Usiikusanye roho yangu pamoja nazo zao wakosaji! Usininyime uzima pamoja nao wauao wenzao! Mikononi mwao yamo mapotovu, mikono yao ya kuume imejaa mapenyezo. Lakini mimi ninaendelea pasipo kosa; kwa kunihurumia nikomboe! Miguu yangu huenda paliponyoka, nimtukuze Bwana katika mikutano. Bwana ni mwanga wangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Bwana ni ngome, nilimpoponea, nimstuke nani? Wafanyao mabaya wanikaribia, wanile nyama zangu, lakini wanisongao nao wanichukiao watakajikwaa, waanguke. Ijapo kikosi kizima kinivizie, moyo wangu hauogopi; vita vikinitokea, ninalo egemeo langu. Hili moja, ninalolitaka sana, namwomba Bwana, nikae Nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu, niutazame na kuuchunguza uzuri wake Bwana Jumbani mwake. Kwani hunifunika kambini kwake, siku ikiwa mbaya; hunificha fichoni penye hema lake akinikweza mwambani. Kwa hiyo sasa kichwa changu kitakuwa kimeinuka, kiwashinde wachukivu wangu wanizungukao; napo penye hema lake ndipo, nitakapomtambikia na kumtolea vipaji vya tambiko vya kumshangilia, nimchezee Bwana ngoma na kumwimbia. Bwana, isikie sauti yangu, ninapokuita, uniwie mpole na kuniitikia! Moyo wangu unakukumbusha neno lako, lile la kwamba: Utafuteni uso wangu! Sasa ninauelekea uso wako, Bwana, kwa kuutafuta. Nawe usiufiche uso wako, usinione! Mtoto wako usimwepuke kwa makali na kumwacha! Wewe ndiwe uliyenisaidia, usinitupe! Mungu aliye wokovu wangu, usiniache! Kwani baba na mama wakiniacha, Bwana hunifikiza kwake. Bwana, nifundishe njia yako na kuniongoza, nifuate mapito yanyokayo, waninyatiao wasinipate! Usinitie mikononi mwao wanisongao! Kwani ndio mashahidi wa uwongo walioniinukia, nao, kusudi wanikorofishe, hunifokea. Lakini ninayetegemea ya kwamba: Nitaona meme ya Bwana katika nchi yao walio hai. Mngojee Bwana, ujipatie nguvu! Ushupaze moyo wako, umngojee Bwana! Wewe Bwana ninakuita, u mwamba wangu, usininyamazie na kuwa kimya, nisije kufanana nao washukao kuzimuni! Zisikie sauti za malalamiko yangu, ninapokulilia nikikuinulia mikono yangu pale Patakatifu Penyewe palipo pako! Usinipokonye pamoja nao wasiokucha, wala pamoja nao wafanyao maovu! Wao husema polepole na wenzao, lakini mioyoni mwao yamo mabaya. Uwape yazipasayo kazi zao na ubaya wa matendo yao, mishahara yao ipatane nayo, mikono yao yatendayo! Ndivyo, utakavyowarudishia yaliyofanyizwa nao! Kwani kazi zake Bwana hawazitambui, wala mikono yake iyatendayo! yawayo yote, kwa hiyo atawavunja, asiwajenge tena. Apasaye kutukuzwa ni Bwana, kwani huzisikia sauti zao malalamiko yangu. Bwana ni nguvu yangu na ngao yangu; moyo wangu ulipomwegemea, nikapata kusaidiwa. Moyo wangu ukamshangilia, nikamwimbia nyimbo za kumshukuru. Bwana ni nguvu yao, walio wake, tena ni ngome imwokoayo aliyempaka mafuta. Waokoe walio ukoo wako na kuwabariki watakaopata fungu kwako! Wachunge na kuwavumilia kale na kale! Mheshimuni Bwana, mlio wana wa Mungu! Mheshimuni Bwana kuwa mtukufu na mnguvu! Liheshimuni nalo Jina lake Bwana lenye utukufu! Mtambikieni Bwana na kuvaa mapambo yapasayo Patakatifu! Sauti ya Bwana husikilika hata baharini, Mungu mwenye utukufu ndiye apigishaye nayo ngurumo. Nako kwenye vilindi vya bahari ndiko, aliko Bwana. Sauti ya Bwana ni yenye nguvu, sauti ya Bwana ni yenye ukuu. Sauti ya Bwana huvunja miangati, kweli Bwana huivunja miangati ya Libanoni akiichezesha, icheze kama ndama, ile ya Libanoni na ya Sirioni icheze kama wana wa nyati. Sauti ya Bwana hutema miali ya moto, Sauti ya Bwana hutetemesha nyika. Bwana aliitetemesha nayo nyika ya kule Kadesi. Sauti ya Bwana huzalisha kulungu, hutikisa miti ya mwituni, matawi yavunjike; kwa hiyo wote waliomo Jumbani mwake humtukuza. Hapo penye mafuriko ya maji Bwana alikaa juu yao; ndivyo, atakavyokaa kuwa mfalme wa kale na kale. Bwana atawapa nguvu walio ukoo wake, Bwana atawabariki walio ukoo wake, wapate kutengemana. Nitakutukuza Bwana, kwani umeniopoa, hukuwapa adui zangu kunifurahia mimi. Bwana Mungu wangu, nilipokulilia, ndipo, uliponiponya. Bwana, umeipandisha roho yangu, itoke kuzimuni; wengine waliposhuka kaburini, ulinirudisha uzimani. Ninyi mmchao Mungu, mwimbieni Bwana wenu! Mshukuruni, mwakumbushe watu utakatifu wake! Kwani makali yake hukaa punde kidogo tu, kuwapa watu uzima ndiko kunakompendeza. Kama jioni tunakwenda kulala wenye kilio, asubuhi kimegeuka kuwa kicheko. Hapo nilipokaa salama nilisema moyoni: Sitatikisika kale na kale. Bwana, uliponitazama kwa kupendezwa ulikuwa umeushikiza mlima wangu, upate nguvu; lakini ulipouficha uso wako, nikawa nimestuka! Ndipo, nilipokulilia, wewe Bwana, Bwana wangu ndiye kweli, niliyemlalamikia: Utapata nini, damu yangu ikimwagwa, nishuke kuzimuni? Mavumbi yatakushukuru nayo, yaitangaze kweli yako? Sikia, Bwana, uniwie mpole! Bwana, nitokee kuwa msaidiaji wangu! Maombolezo yangu umeyageuza kuwa mashangilio, ukanivika nguo za mchezo ukinivua gunia, roho yangu iliyotukuka hivyo, na ikuchezee, isinyamaze. Bwana Mungu wangu, kale na kale nitakushukuru. Wewe Bwana, nimekukimbilia, sitatwezeka kale na kale. Kwa kuwa mwenye wongofu na uniponye! Nitegee sikio lako, unisaidie upesi! Niwie mwamba wenye nguvu na nyumba yenye boma! Ndivyo, utakavyopata kuniokoa. Kwani mwamba wangu na boma langu ndiwe wewe, kwa ajili ya Jina lako utaniongoza, unipeleke. Unitoe katika tanzi, walilonitegea! Kwani aliye nguvu yangu ndiwe wewe. Roho yangu naiweka mikononi mwako; Bwana uliye Mungu wa kweli, umenikomboa. Nawachukia waangaliao mizimu iliyo ya uwongo tu, mimi ninayemwegemea, ndiye Bwana. Nitashangilia na kuufurahia upole wako, kwa kuwa umeutazama ukiwa wangu, ukayatambua nayo masongano ya roho yangu. Hukunitia mikononi mwao walio adui zangu, miguu yangu huipatia papana pa kusimamia. Niwie mpole, Bwana! Kwani nimesongeka, macho yangu yamenyauka kwa uchungu, nayo roho vilevile pamoja na mwili. Kwani siku zangu zimeishia kwa masikitiko, miaka yangu nayo kwa kupiga kite, nguvu yangu imepondeka kwa manza, nilizozikora, hata mifupa yangu haina kiini. Nikawa wa kufyozwa tu kwao wanisongao, hata kwa wenzangu wa kukaa nao ni vivyo hivyo, nao rafiki zangu ninawatia woga, wanionao njiani hunikimbia. Nimesahauliwa mioyoni mwao kama mfu, nikawa kama chombo kilichovunjika. Nikasikia wengi, wakinong'onezana: Pande zote pia anastukwia tu; wakanilia njama wote pamoja, wakawaza, ndivyo waone njia ya kunitoa roho. Lakini mimi ninayemwegemea, ndiye Bwana, Mungu wangu ndiwe wewe! Hii naungama. Mikononi mwako ndimo, siku zangu za kuwapo zilimo; niponye na kunitoa mikononi mwao adui zangu wanikimbizao! Uangaze uso wako, mtumishi wako auone! Kwa upole wako na uniokoe! Bwana, usiniache, nisije kutwezwa, kwani nikakulilia; sharti watwezwe wao wasiokucha, na waje kuzimuni kuyamazia huko! Midomo yenye uwongo sharti ifumbwe kuwa kimya, kwani mwongofu wamemtolea meneno ya kumkorofisha, kwa majivuno yao wakambeza. Ninayastaajabu mema yako, jinsi yalivyo mengi, umeyalimbikia wao wakuogopao, nao wakukimbiliao huwapa machoni pa watu. Mafichoni kwa uso wako unawaficha, watu wakiwatolea ukali; ukawafunika chumbani ndani, ndimi zao zikiwagombeza. Bwana na atukuzwe! Kwani amenistaajabisha, akaniweka mjini mwenye nguvu kwa upole wake. Nami kwa woga wangu nilikua nimesema: Nimetupwa, niondoke penye macho yako, yasinione tena. Lakini malalamiko yangu umeyasikia kweli hapo, nilipokulilia, unisaidie. Mpendeni Bwana, ninyi yote mmchao! Bwana huwalinda wamtegemeao. Lakini wafanyao majivuno huwalipisha, asisaze hata kidogo. Jipeni mioyo, mpate nguvu, nyote mnaomngojea yeye Bwana! *Mwenye shangwe ndiye aondolewaye mapotovu, naye aliyefunikwa makosa yake. Mwenye shangwe ni mtu, Bwana asiyemhesabia manza, asiyekuwa na udanganyifu rohoni mwake. Kwani nilipoyanyamazia, mifupa yangu ikanyauka kwa hivyo, nilivyopiga kite mchana kutwa. Kwani mkono wako ulinilemea mchana na usiku, kiini cha mifupa kikakauka kama maji penye kiangazi. Ndipo, nilipokuungamia makosa yangu, nazo manza, nilizozikora, sikuzifunika; nikasema: Nitamwungamia Bwana mapotovu yangu; ndipo, wewe uliponiondolea manza, nilizozikora kwa kukosa. Kwa hiyo kila akuchaye atakubembeleza, siku zitakapotimia; maji mengi yatakapofurika hayatamfikia. Wewe nidwe ficho langu, utanilinda, nisisongeke; utanipa, nikushangilie po pote kwa kuniponya.* Nitakufundisha na kukuonyesha njia, utakayoishika; macho yangu yatakuelekeza, nikikupa shauri. Msiwe kama farasi au nyumbu wakosao akili! Wasipotiwa hatamu na mafungo hawaji kwako. Maumivu yake asiyemcha Mungu ndiyo mengi, lakini amwegemeaye Bwana hugawiwa mengi, yamzunguke. Mfurahieni Bwana na kumshangilia, ninyi waongofu! Nyote mnyokao mioyo, pigeni vigelegele! Pigeni vigelegele, ninyi waongofu, kwa kuwa naye Bwana! Kumtukuza na kumsifu kunawapasa wanyokao mioyo. Mshukuruni Bwana na kupiga mazeze! Mpigieni nayo mapango yenye nyuzi kumi! Mwimbieni wimbo mpya na kupiga shangwe zilizo nzuri mkizipatanisha nayo marimba! Kwani Bwana ayasemayo hunyoka, nayo yote ayafanyayo hutimia kweli. Hupenda mashauri yaongokayo, nchi imejaa magawio yake Bwana. Kwa neno lake Bwana mbingu zilifanyika, nayo majeshi yao yote yakatokea, alipopuzia na kinywa chake. Maji ya bahari huyakusanya, kama yamo chunguni, navyo vilindi huviweka mahali pao. Sharti zimwogope Bwana nchi zote, nao wote wakaao ulimwenguni sharti wamche. Kwani Yeye ayasemayo mara huwapo; Yeye ayaagizayo hutokea papo hapo. Bwana huyavunja mashauri yao wamizimu, huyatengua mawazo yao makabila ya watu. Shauri lake Bwana husimama kale na kale, mawazo ya moyo wake hutimilia vizazi kwa vizazi. Wenye shangwe ndio, Bwana aliowawia Mungu, nalo kabila la watu, aliowachagua, wawe fungu lake. Bwana huchungulia toka mbinguni, huwatazama wote pia walio wana wa watu. Kwenye kao lake, alikotua, huwaangalia wote wakaao nchini. Yeye ndiye aliyeiumba mioyo yao wote, naye ndiwe anayeyapambanua matendo yao yote. Hakuna mfalme aokolewaye na nguvu zake nyingi, wala fundi wa vita aponaye kwa uwezo wake mwingi. Farasi nao ni wa bure, hawashindi, nguvu zao nyingi haziponyi mtu. Utaliona jicho la Bwana, likiwatazama wamwogopao, ndio waingojeao huruma yake, aziokoe roho zao katika kufa, hata siku za njaa awatunze. Roho zetu zinamngoja yeye Bwana, ndiye msaada wetu na ngao yetu. Kwa hiyo mioyo yetu inamfurahia, kwani Jina lake takatifu tunaliegemea. Wema wako, Bwana, utukalie! Hivyo ndivyo, tunavyovingojea toka kwako. *Nitamtukuza Bwana siku zote, mashangilio yake yakae midomoni mwangu pasipo kukoma. Roho yangu inayejivunia, ndiye Bwana, wakiwa na wayasikie, wapate kufurahi. Mkuzeni Bwana pamoja nami! Na tulitukuze pamoja jina lake! Nilipomtafuta Bwana, akaniitikia, katika woga wangu wote akaniponya. Wanaomtazamia huchagamka, maana nyuso zao hazitatwezwa. Kama yuko mnyonge aliyeita, Bwana husikia, katika masongano yake yote humwokoa. Malaika wa Bwana huwakingia wao wamwogopao, huwa kwao pande zote, apate kuwaponya. Onjeni, mwone, ya kuwa Bwana ni mwema! Mwenye shangwe ni mtu amkimbiliaye.* Mwogopeni Bwana, ninyi watakatifu wake! Kwani kwao wamwogopao hakuna ukosefu. Wana wa simba hukosa na kuona njaa, lakini hakuna chema, watakachokikosa wamtafutao Bwana. Njoni, ninyi wana, mnisikilize, kumwogopa Bwana ndiko, nitakakowafundisha. Mtu apendezwaye na uzima yuko wapi? naye apendaye siku za kuona mema? Uulinde ulimi wako, usiseme mabaya, nayo midomo yako, isiseme madanganyifu! Yaliyo mabaya yaepuke, ufanye mema! Tafuta penye utengemano, upakimbilie! Macho ya Bwana huwatazama walio waongofu, masikio yake huvisikiliza vilio vyao. Uso wa Bwana huwapingia wafanyao mabaya, awang'oe, wasikumbukwe tena katika nchi. Waongofu wanapoita, Bwana huwasikia, katika masongano yao yote hutaka kuwaponya. Bwana yuko karibu kwao waliovunjika mioyo, wapondekao roho huwaokoa. Kweli, mabaya mengi humpata aliye mwongofu, lakini katika hayo yote Bwana humponya. Nayo mifupa yake yote huiangalia, hata mmoja miongoni mwao usivunjike. Ubaya utamwua asiyemcha Mungu, nao wachukiao wongofu watakuwa wenye manza; lakini roho zao watumishi wake Bwana huzikomboa, wao wote wamkimbiliao, wawe watu wasio wenye manza. Bwana, gombana nao wanigombezao! Pigana nao wanipiganishao! Shika ngao na kingio! Inuka, unisaidie! Chezesha mkuki, uwakinge wao wanikimbizao! Iambie roho yangu kwamba: Wokovu wako ni mimi. Sharti watwezwe kwa kuumbuka waitafutao roho yangu, sharti warudi nyuma na kuinamisha vichwa waniwaziao vibaya; sharti wawe kama makapi, yakipatwa na upepo, malaika wa Bwana akiwakumba, waanguke. Njia yao sharti iwe yenye giza pamoja na utelezi, atakapowakimbiza malaika wa Bwana. Kwani wamenitegea tanzi lao, linikamate, pasipo sababu yo yote, wakaichimbia roho yangu miina pasipo sababu yo yote. Na uwajie mwangamizo wa kustusha, ambao walikuwa hawaujui, nalo tanzi lao, walilolitanda, liwakamate wao; huo mwangamizo wa kustusha ukiwapata, na waangushwe nao. Ndipo, roho yangu itakapopiga vigelegele kwa kuwa na Bwana, na kuushangilia wokovu, iliouona. Ndipo, itakaposema nayo mifupa yangu yote: Bwana, afananaye nawe yuko wapi? Unamponya mnyonge mkononi mwake yeye ampitaye nguvu, kweli huponya mnyonge na mkiwa mikononi mwao wamnyang'anyao. Mashahidi wa ukorofi wananiinukia, wananiuliza mambo, nisiyoyajua. Mema, niliyowatendea, wanayalipa na kunifanyizia mabaya, ukiwa wa kuwa peke yake uipate roho yangu. Lakini vazi langu mimi lilikuwa gunia hapo, walipougua, nikajisumbua kwa kufunga na kwa kuwaombea na kujipiga kifua. Niliwaendea, kama ni ndugu yangu, niliyempenda kweli, kama amwombolezeaye mama niliinamisha kichwa kwa kusikitika. Lakini wao hulifurahia anguko langu wakikusanyika; kweli walikusanyika kwa ajili yangu mimi, nao nisiowajua wananitukana pasipo kukoma. Kwao wenye ulafi wa matusi huyafyoza nayo ya Kimungu, kisha hukereza meno kwa ajili yangu mimi. Bwana, utawatazama tu mpaka lini? Irudishe roho yangu uzimani, wasiimalize! Nitoe kwenye wana wa simba! Kwani niko peke yangu. Kwa hiyo nitakushukuru, wengi wakutanikapo, na kukuimbia kwenye watu walio wenye nguvu. Wapendao uwongo wasinifurahie, wala wasinitazame na jicho baya wanichukiao bure! Kwani yawezayo kutupatanisha hawayasemi, nao walio watulivu katika nchi huwawazia mambo ya udanganyifu. Wananiasamia sana vinywa vyao kwa kusema: Macho yetu yamekuona! Weye! Weye! Bwana, umeyaona, usiyanyamazie! Usinikalie mbali, Bwana wangu! Amka! Inuka, uniamulie! Mungu wangu na Bwana wangu, unigombee! Niamulie kwa wongofu wako, Bwana Mungu wangu, wasinifurahie! Wasiseme mioyoni mwao: Weye! Ndivyo vinavyotupendeza! Wala wasiseme: Tumemmeza! Sharti watwezwe wakiumbuliwa wote pamoja waliofurahiwa na mabaya yaliyonipata, sharti wavikwe soni, nyuso ziwaive waliojikuza na kuninyenyekeza. Lakini wao waliopendezwa na wongofu wangu sharti wapige vigelegele kwa kufurahiwa! Sharti waseme pasipo kukoma: Mkuu ni Bwana, mtumishi wake akikaa na kutengemana, hupendezwa. Ulimi wangu sharti uusimulie wongofu wako, ukusifu wewe siku zote! Upotovu husema ndani moyoni mwake yeye asiyemcha Mungu, kumwogopa Mungu hakupo machoni pake. Kwani hujidanganya kwamba: Manza, nilizozikora, macho yake hayataziona, asichukizwe nazo. Maneno, ayasemayo, ni maovu, tena madanganyifu; hukataa kuonyeka, asifanye mema. Maovu ndiyo, ayawazayo hapo, anapolala, hujisimamisha katika njia isiyo njema, nacho kilicho kibaya hana mwiko nacho. Bwana, mpaka mbinguni unafika wema wako. welekevu wako unayafikia nayo mawingu. Welekevu wako unasimama kama milima ya Mungu, maamuzi yako nayo hujenga, kama vilindi vijengavyo, Bwana, unawaokoa wote, watu na nyama. Kuliko wema wako, Mungu, hakuna chenye kiasi, wana wa watu hukikimbilia kivuli cha mabawa yako. Unono wa nyumba yako wanaushiba, navyo vinywaji vya urembo, unavyowanywesha, ni vingi kama vya mto. Kwani kwako kiko kisima chenye uzima, namo mwangani mwako tunauona mwanga. Ueneze wema wako kwao wakujuao nao wongofu wako kwao wanyokao mioyo! Miguu yao wajivunao isinijie, wala mikono yao wasiokucha isinifukuze! Kwao wafanyao maovu itakuja siku, watakapokuwa wameanguka, watakuwa wamebwagwa, wasiweze kuinuka tena. Kwa ajili yao watendao mabaya usijichafushe moyo, wala wafanyao mapotovu usiwaonee wivu! Kwani hunyauka upesi kama majani, kama machipuko mazuri ya uwandani watakauka. Mwegemee Bwana, ufanye mema! Kaa katika nchi, ujilishe mambo yaelekeayo! Furaha zilizoko kwake Bwana na zikutoshe! Naye ndiye atakayekupa, moyo wako uyatakayo. Acha, Bwana akuchagulie njia, utakayoishika! Mwegemee tu, yeye atafanya! Atautokeza wongofu wako, uwe kama mwanga; nayo mashauri yako yataangazika kama jua la mchana. Mnyamazie Bwana na kumngoja! Mwenzio akiona mema njiani, usiwake moto, ijapo awe mtu afanyaye madanganyo! Tuliza ukali, uache kufoka! Usiwake moto, usije kukukosesha! Kwani wafanyao mabaya watang'olewa, lakini wao wamngojeao Bwana wataitwaa nchi. Bado kidogo asiyemcha Mungu atakuwa hayupo tena; hapo, utakapopachungulia mahali pake, patakuwa hapapo. Lakini wapole ndio watakaoitwaa nchi, kwa kupata matengemano mengi furaha zitawatosha. Asiyemcha Mungu huwaza, jinsi atakavyomponza mwongofu, hukereza meno yake kwa ajili yake yeye. Lakini Bwana humcheka kwa kupaona, siku yake itakapofika. Wasiomcha Mungu huchomoa panga na kuzipinda pindi zao, wapate kuwaangusha walio wanyonge na wakiwa, nao wafuatao njia zinyokazo wawachinje. Lakini panga zao zitaichoma mioyo yao wenyewe, nazo pindo zao zitavunjika. Mema machache ya mwongofu ni mali, nazo zinapita mafuriko mengi yao wasiomcha Mungu. Kwani mikono yao wasiomcha Mungu itavunjwa, lakini wao walio waongofu Bwana huwashikiza. Bwana huzijua siku zao wamchao, nayo mafungu yao yatakuwapo kale na kale Siku zitakapokuwa mbaya, hawatatwezeka, ila watashiba vema nazo siku za njaa. Kwani wasiomcha Mungu wataangamia, nao wamchukiao Bwana watatoweka, kama uzuri wa majani ya uwandani unavyotoweka; watatoweka kweli kama moshi. Asiyemcha Mungu hukopa, asiweze kulipa; mwongofu huweza kugawia na kuwapa watu. Kwani wabarikiwao naye Bwana huitwaa nchi, lakini waapizwao naye watang'olewa. Mwendo wa mtu unashupazwa naye Bwana, akiwa anapendezwa na njia, yule anayoishika. Kama anajikwaa, hataangushwa chini, kwani Bwana humshika mkono wake. Nalikuwa kijana, nikaja kuwa mzee, lakini sijaona bado mwongofu aliyeachwa peke yake, wala watoto wake wakiombaomba chakula. Kila siku anaweza kugawia wengine, hata kuwakopesha, nao watoto wake hubarikiwa. Ondoka pabaya ufanye mema! Ndivyo, utakavyokaa kale na kale. Kwani Bwana huyapenda yaongokayo, hatawaacha kabisa wao wamchao, watakuwa wamelindwa kale na kale, lakini watoto wao wasiomcha watang'olewa. Walio waongofu wataitwaa nchi, wakae humo kale na kale. Kinywa chake mwongofu hueleza yenye werevu wa kweli, ulimi wake husema yaongokayo. Maonyo ya Mungu wake yamo moyoni mwake, kwa hiyo hatikisiki atakapokwenda pote. Asiyemcha Mungu humwotea mwongofu akitafuta kumwua. Lakini Bwana hatamwacha mkononi mwake; hata akihukumiwa naye yule, hatamhesabu kuwa mbaya. Ishike njia yake Bwana na kumngojea! Ndipo, atakapokukweza, uitwae nchi; nako kung'olewa kwao wasiomcha utakufurahia. Nimeona mtu asiyemcha Mungu, akawa mkorofi, akawa mnene sana kama mtamba wenye majani mengi. Lakini nilipomtazama, siku zilipopita, alikuwa hayupo, nikamtafuta, lakini hakuoneka. Jilinde, ukae na kumcha Mungu, uyatazamie yanyokayo! Kwani mtu aliye hivyo mwisho hutengemana. Lakini wapotovu huangamizwa wote pamoja, mwisho wao wasiomcha Mungu ni kung'olewa. Wokovu wao waongofu hutoka kwake Bwana, yeye ni nguvu yao siku, wanaposongeka. Bwana huwasaidia na kuwaopoa, huwaopoa mikononi mwao wasiomcha Mungu; kwa kuwa humkimbilia, huwaokoa. Bwana, usinipatilize kwa ukali wako, wala kwa machafuko yako yenye moto usinichapue! Kwani mishale yako imenichoma, nao mkono wako umenilemea. Hakuna kilicho kizima mwilini mwangu kwa ukali wako ulionitokea. Wala fupa lisilopatwa na ugonjwa haliko kabisa kwa ajili yao hayo, niliyoyakosa. Manza, nilizozikora, zinanirudia, nizitwike kichwani, lakini kwa kuwa mzigo upitao nguvu zangu zinanilemea. Madonda yangu yananuka kwa usaha mwingi kwa hivyo, nilivyokuwa mwenye upumbavu. Kwa kupindika sanasana nimepotoka, mchana kutwa ninatembea kwa kusikitika. Kwani viuno vyangu vinazidi kuchomwa na moto wa machungu, hakuna kilicho kizima mwilini mwangu. Nimegeuka kuwa mwembamba kwa kupondeka sanasana, moyo ukizidi kunipiga mno, ninalia. Bwana, unayajua yote, niyatakayo, hata ninavyopiga kite, havikujificha kwako. Moyo wangu unatetemeka kwa kutokwa na nguvu, nilizokuwa nazo, nao mwanga wa macho yangu haumo tena mwangu. Wapenzi wangu na rafiki zangu husimama mbali kwa kuviona hivyo, ninavyopatilizwa; nao walio ndugu zangu husimama mbali. Wanaonitakia roho yangu wananitegea, wanaotafuta, watakavyoniangamiza vibaya, wanasema mapotovu, wananong'onezana madanganyifu mchana kutwa. Lakini mimi niko kwao kama kiziwi, nisiyasikie, au kama bubu asiyefumbua kinywa chake; ndivyo, nilivyo kwao. Kweli ninafanana na mtu asiyesikia, asiyeweza kubisha na kinywa chake. Kwani wewe Bwana ndiwe, niliyekungojea; wewe utawajibu, Bwana Mungu wangu. Kwani nimesema: hawatafurahi kamwe na kunicheka; kama mguu wangu ungejikwaa, wangejivuna na kunibeza. Kwani kuvunjika kuko karibu kwangu mimi, maumivu yangu hayakomi hata kidogo. Manza, nilizozikora, ninaziungama, kwa kuyasikitikia hayo, niliyoyakosa. Lakini adui zangu ni wenye uzima, nguvu za miili wanazo, nao wanaonichukia bure ndio wengi. Mema, niliyowafanyizia, wanayalipa na kunifanyizia mabaya wananipingia, kwa sababu ninayakimbilia yaliyo mema. Usiniache, wewe Bwana! Mungu wangu, usinikalie mbali! Piga mbio, unisaidie, wewe Bwana, wokovu wangu! Nilisema: Nitaziangalia njia zangu, nisiukoseshe ulimi wangu; nacho kinywa changu nitakiangalia na kukifumba, asiyemcha Mungu akingali yuko mbele yangu. Nikanyamaza kimya, sikusema neno; lakini hakuna chema, nilichokiona, maumivu yakazidi kunila. Moto ukauchoma moyo wangu kifuani mwangu, nao huo moto ukawaka na nguvu, nilipoyawaza hayo; ndipo, nilipoufungua ulimi, na useme: *Bwana, nijulishe mwisho utakaonipata! Niujue nao mpaka wa siku zangu, ziliokatiwa! Tena ni mbali gani kuufikia! Ya kuwa mimi ni mpitaji tu, na niyajue! Tazama, siku zangu, ulizonipa, ni zenye upana kama wa kiganja tu; mbele yako nipo kama mtu asiyekuwapo. Kweli kila mtu, ijapo awe mwenye nguvu, ni mvuke tu. Mtu hujiendea kama kivuli, mambo ya ovyoovyo huyapigia makelele, hamjui atakayezipata mali zake, lakini huzilimbika. Sasa ningojee nini, Bwana wangu? Ninakungojea wewe peke yako. Katika mapotovu yangu yote niopoe, lakini usinitoe kuwa wa kusimangwa nao wapumbavu! Nitanyamaza tu, nisikifumbue kinywa changu, kwani wewe ndiwe uliyeyafanya. Liondoe patilizo lako, linitoke! Kwa mapigo ya mkono wako mimi nimemalizika. Ukimtisha mtu na kumchapua kwa ajili ya manza, unautowesha uzuri wake, kama nondo anavyofanya. Kweli kila mtu aliopo ni mvuke tu. Bwana, yasikie maombo yangu! Vilio vyangu sharti vifike masikioni mwako! Nayo machozi yangu usiyanyamazie! Kwani mimi ni mgeni tu apangaye kwako, kama baba zangu wote walivyokuwa. Fumba macho, yasinione, uso uning'ae, nikingali sijaenda bado, nisiwepo tena!* Nimekuwa nimemngojea yeye Bwana, naye akaniinamia, akakisikiliza kilio changu. Akanitoa katika mwina uangamizao, nako kwenye matope yazamishayo, akaisimamisha miguu yangu juu mwambani, nao mwendo wangu akaushupaza. Akanipa kinywani mwangu wimbo mpya, nao ni wa kumshangilia Mungu wetu. Wengi wataviona na kuogopa, kisha nao watamwegemea huyu Bwana. Mwenye shangwe ni mtu amtumiaye Bwana kuwa egemeo lake, asiyewageukia wajivunao, wala wao wanaodanganya na kutumikia uwongo! Bwana Mungu wangu, uliyoyafanya wewe, ni mengi, ni mataajabu yako na mawazo yako yaliyotutokea; hakuna anayefanana nawe wewe. Ninataka kuyatangaza na kuyasimulia, ijapo yawe mengi, yasihesabike. Ng'ombe na vyakula vya tambiko hakupendezwa navyo, lakini umenizibua masikio yangu; ng'ombe za tambiko zinazoteketezwa nzima navyo vipaji vya tambiko vya kulipa makosa hukuvitaka. Ndipo, niliposema: tazama, ninakuja! Mambo yangu yamekwisha kuandikwa katika kitabu cha kuzingwa. Kuyafanya, uyatakayo wewe, Mungu wangu, kunanipendeza, nayo Maonyo yako yamo ndani moyoni mwangu, nikatangaza yaongokayo, wengi walipokusanyika; itazame midomo yangu, sikuifunga, wewe ulio Bwana unavijua. Wongofu wako sikuufunika ndani moyoni mwangu, ila welekevu wako na wokovu wako nikausimulia, wala sikuuficha wema wako na ukweli wako, wengi walipokusanyika. Huruma zako, wewe Bwana, usininyime, wema wako na ukweli wako unilinde siku zote! Kwani makosa yasiyohesabika yalinizunguka, manza, nilizozikora, zikanirudia, nisiweze kuziona zote, ni nyingi sana kuliko nywele za kichwani pangu; ndipo, moyo wangu ulipojiendea, ukanipotelea. Na vikupendeze, Bwana, kuniopoa! Bwana, piga mbio, unisaidie! Sharti wapatwe na soni kwa kutwezwa wao wote pamoja walioitafuta roho yangu, waiangamize! Sharti warudishwe nyuma, nyuso ziwaive kwa soni waliopendezwa na mabaya yaliyonipata mimi. Sharti waustukie ukiwa wao na kuona soni wale walioniambia: Weye! Weye! Sharti wachangamke na kufurahiwa wote wakutafutao! Waupendao wokovu wako waseme pasipo kukoma: Mkuu ni Bwana! Ijapo, niwe mnyonge na mkiwa, Bwana hunikumbuka; msaada wangu na mwokozi wangu ndiwe wewe, Bwana; Mungu wangu, usinikawilie! Mwenye shangwe ni mtu atunzaye mnyonge. Naye atakapopatwa na kibaya, Bwana atamwokoa. Bwana atamlinda, atampa uzima, aone mema nchini; hutamtoa, adui zake wampate kwa kumtamani. Akilala kitandani kwa kuugua, Bwana atamshikiza, amwuguze na kumtandikia vema katika ugonjwa wake wote. Mimi nasema: Bwana, nihurumie! Iponye roho yangu! Kwani nimekukosea. Adui zangu wananisema vibaya kwa kwamba: Itakuwa lini, atakapokufa, jina lake liangamie? Kama mtu anakuja kunikagua, hujisemea ovyo tu, lakini moyo wake huokota ayaonayo kuwa mapotovu, kisha anatoka nje, ayasema. Wote wanichukiao hunong'onezana pamoja, watakayonifanyizia, ni mabaya tu, wanayoniwazia kwa kwamba: Jambo lisilopona limemkaza, hivyo, anavyolala, hatainuka tena. Hata mwenzangu wa uchale, niliyemwegemea kwa moyo, naye anayeula mkate wangu, hunipiga mateke. Lakini wewe Bwana, nihurumie na kuniinua, nipate kuwalipiza! Hapo ndipo, nitakapotambua, ya kuwa umependezwa nami, adui yangu asipoweza tena kunipigia yowe. Kwa hivyo, mimi ninavyokucha kwa moyo wote, unanishikiza, ukanipa kusimama usoni pako kale na kale. Bwana Mungu wa Isiraeli, na atukuzwe kama huko kale, vivyo nazo siku zitakazokuwa kale na kale! Amin. Amin. *Kama kuro anavyolilia maji ya mtoni, ndivyo, roho yangu inavyokulilia wewe, Mungu. Roho yangu ina kiu ya kunywea kwake Mungu, kwake yeye aliye Mungu Mwenye uzima. Itakuwa lini, nitakapoonekana usoni pake Mungu? Machozi yangu ndio chakula changu mchana na usiku, maana watu huniambia kila siku: Mungu wako yuko wapi? Ndipo, ninapoumimina moyo wangu ndani yangu kwa kuvikumbuka hivyo, nilivyokwenda na kikosi cha watu nilipowaongoza na kuwapeleka Nyumbani kwa Mungu, wao wakipiga vigelegele vya kumshukuru, wakawa kundi kubwa la watu waliokula sikukuu. Mbona unajihangaisha, roho yangu, ukivuma ndani yangu? Mngoje Mungu na kumtazamia! Kwani siku itakuja, nitakapomshukuru kwa kuokolewa nao uso wake. Roho yangu inajihangaisha humu ndani yangu, kwa sababu hii ninakukumbuka huku, niliko katika nchi za Yordani kwenye Hermoni nako mlimani kwa Misari. Maanguko yako ya maji yakinguruma, vilindi vinaitana, kisha mafuriko na mawimbi yako yote huja kunifunika. Mchana Bwana na aniagizie upole wake, usiku nipate kumwimbia na kumwomba Mungu anipaye uzima. Nitamwambia Mungu aliyemwamba wangu: Mbona umenisahau? Mbona sina budi kwenda na kusikitika, adui anaponisonga? Mifupa yangu inakuwa imepondeka sana, wanisongao wakinitukana, wakiniambia kila siku: Mungu wako yuko wapi? Mbona unajihangaisha, roho yangu, ukivuma ndani yangu? Mngoje Mungu na kumtazamia, kwani siku itakuja, nitakapomshukuru kwa kuokolewa nao uso wake.* Niamulie, Mungu, ukinigombea kondo yangu kwao wasionipenda! Niopoe mikononi mwao wenye uwongo namo mwao wapotovu! Kwani wewe Mungu uliye nguvu yangu, mbona umenitupa? Mbona sina budi kwenda na kusikitika, adui anaponisonga? Tuma mwanga wako na kweli yako, ije kuniongoza na kunipeleka kwenye mlima wako mtakatifu, Kao lako liliko. Niingie mwenye meza ya kumtambikia Mungu wangu, ni yule Mungu, ninayemfurahia na kumpigia vigelegele. Nitakushukuru na kukupigia zeze, Mungu uliye Mungu wangu. Mbona unajihangaisha, roho yangu, ukivuma ndani yangu? Mngoje Mungu na kumtazamia, kwani siku itakuja, nitakapomshukuru kwa kuokolewa nao uso wake. Mungu, tulisikia na masikio yetu, baba zetu wakituambia: Ulitenda tendo siku zao, hata siku za kale. Wewe kwa mkono wako uliwafukuza wamizimu, ukawaweka pao, ukaangamiza makabila ya watu, upate pa kuwaenezea. Kwani nchi hawakuitwaa kwa nguvu za panga zao, wala mikono yao siyo iliyowashindisha, ila mkono wako wa kuume na mwanga wa uso wako ndio uliovifanya kwa kupendezwa nao. Wewe, Mungu, ndiwe uliye mfalme wangu; uagize wokovu, umjie Yakobo! Kwa nguvu zako tutawakumba watusongao, waanguke; kwa nguvu za Jina lako tutawapiga mateke watuinukiao. Kwani siutegemei upindi wangu, kweli sio, ninaoujetea, wala upanga wangu sio uniokoao. Kwani wewe ulituokoa mikononi mwao watusongao, nao watuchukiao uliwatia soni. Mungu tunamwimbia siku zote, Jina lako tunalishukuru kale na kale. Na sasa umetutupa na kututia soni, maana hukutoka pamoja navyo vikosi vyetu, Ukaturudisha nyuma mbele yao watusongao, nao watuchukiao wakajipatia mateka; ukatutoa, kama tu kondoo, tuwe chakula, ukatutawanya kwao walio wamizimu. Walio ukoo wako umewauza kwa mali zisizo mali, lakini kwa hayo malipo yao hakuna ulichokipata. Ukatutia soni kwao, tuliokaa nao, tukafyozwa na kusimangwa nao waliotuzunguka. Ukatuweka kuwa kama fumbo kwa wamizimu, makabila ya watu hututingishia vichwa vyao. Siku zote hayo mabezo yapo machoni pangu; naufunika uso wangu kwa kuona soni nikizisikia sauti zao wanifyozao pamoja na kunitukana, nikimwona adui anitakaye, apate kujilipiza. Haya yote yametupata, lakini hatukukusahau, wala hatukulivunja Agano lako, wala mioyo yetu haikurudi nyuma, wala miguu haikuondoka katika njia yako. Nako, mbwa wa mwitu wanakokaa, ukatuponda, ukatufunika na giza kama la kufa. Kama tungekuwa tumelisahau Jina la Mungu, au kama tungekuwa tumemwinulia mungu mgeni mikono yetu, Mungu asingeyaumbua mambo hayo? Kwani yeye huyajua nayo mawazo yajifichayo moyoni. Kumbe ni kwa ajili yako wewe, tukiuawa kila siku, tukihesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa tu! Amka! Sababu gani umelala usingizi, Bwana wangu? Inuka! Usinitupe kale na kale! Sababu gani unauficha uso wako? Umeyasahau maumivu yetu yatusongayo? Kweli roho zetu zimeinamishwa kulala uvumbini, nayo miili yetu imegandamiana na mchanga wa chini. Mwenye msaada, inuka, uje kwetu! Kwa ajili ya huruma yako tukomboe! Moyo wangu umefurika, utunge maneno mema; kwa kumfanyizia mfalme kazi mimi ninayesema. Ulimi wangu ni kalamu ya fundi ajuaye kuandika. Wewe unawashinda wana wa watu kwa uzuri wako. Utu umeenezwa midomoni mwako, kwa hiyo Mungu atakubariki kale na kale. Funga upanga wako kiunoni, wewe mshindaji! Maana ndio pambo lako na urembo wako. Hilo pambo lako na likupe kumaliza kazi! Gombea tu mambo ya kweli na ya upole nayo ya wongofu! Ndivyo, kuume kwako kutakavyokufundisha matendo yatishayo. Mishale yako nayo ni mikali; kwa hiyo makabila ya watu yatakuangukia chini, kwani huichoma mioyo yao adui za mfalme. Mungu, kiti chako cha kifalme kiko kale na kale pasipo mwisho, nayo fimbo ya ufalme wako ndiyo fimbo inyoshayo mambo ya watu. Ulipenda wongofu, ukachukia upotovu. Kwa hiyo Mungu aliye Mungu wako alikupaka mafuta, haya mafuta ni ya kufurahisha kuliko yale ya wenzio. Mavazi yako yote hunukia manemane na udi, hata marashi, kwenye majumba yaliyopambwa na pembe mazeze yanakufurahisha. Humo mna watoto wa kike wa kifalme, uliowapamba vizuri, naye mkeo wa kifalme yuko kuumeni kwako, huwa mwenye mapambo ya dhahabu ya Ofiri. Sikia mwanangu, uviangalie! Niinamishie sikio lako! Sharti uusahau ukoo wako na nyumba ya baba yako! Itakapokuwa, mfalme akutake kwa uzuri wako, basi, kwa kuwa yeye ni bwana wako, sharti umwangukie! Wanawake wa Tiro watakutokea usoni, wakupe matunzo, nao wenye mali wa ukoo huu watajipendekeza kwako. Mwana wa kike wa mfalme yumo nyumbani mlimo na utukufu, nyuzi za dhahabu tu ndizo zilizoyafuma mavazi yake; akivaa nguo za rangi nzuri anapelekwa kwa mfalme, nao watoto wa kike wenzake wamfuatao nyuma wanapelekwa kwako. Katikati ya wapiga shangwe na vigelegele watasindikizwa, waje jumbani mwa mfalme kuwa humo. Hapo, baba zako walipokuwa, watakuwapo wana wako wa kiume, utawaweka kuwa wakuu katika nchi zote. Nitalikumbusha Jina lako kwa vizazi vyote vitakavyokuwa, kwa sababu hii makabila yote ya watu watakushukuru kale na kale, *Mungu ni boma letu la kukimbilia, ni msaada wetu, tuliouona katika masongano kuwa wa kweli. Kwa hiyo hatuogopi, ijapo nchi iondoke, ijapo milima ianguke baharini ndani. Hata bahari ikivuma sana na kukuza mawimbi yake, mpaka milima itetemeke kwa kuumuka kwao: Bwana Mwenye vikosi yuko, yuko pamoja nasi, ngome yetu yenye nguvu ni Mungu wa Yakobo. Uko mto wa kuufurahisha mji wa Mungu kwa vijito vyake, nayo makao matakatifu yake Alioko huko juu yamo humo. Mungu mwenyewe yumo mwake, hautatetemeshwa, Mungu huusaidia, kunapokucha asubuhi. Wamizimu walichafuka, ufalme wao ukatikisika, napo hapo, ngurumo yake yeye iliposikilika, nchi ikayeyuka. Bwana Mwenye vikosi yuko, yuko pamoja nasi, ngome yetu yenye nguvu ni Mungu wa Yakobo. Njoni, mzitazame kazi zake yeye Bwana aletaye maangamizo katika nchi yaliyo hivyo! Kisha huvikomesha vita nako huko mapeoni kwa nchi akizivunja pindi na kuikatakata mikuki, akiyaunguza magari motoni. Acheni, mjue, ya kuwa Mungu ndio mimi! Nitatukuka kwenye wamizimu, nitatukuka nchini. Bwana Mwenye vikosi yuko, yuko pamoja nasi, ngome yetu yenye nguvu ni Mungu wa Yakobo.* Makabila yote ya watu, pigeni makofi! Mwimbieni Mungu kwa shangwe na kumpigia vigelegele! Kwani Bwana alioko huko juu huogopesha, ni mfalme mkubwa azitawalaye nchi zote. Aliteka makabila ya watu, watutii, nazo koo nzima, zituangukie miguuni. Akatuchagulia fungu, liwe letu; ndilo, mpendwa wake Yakobo ajivunialo. Mungu alipaa na kushangiliwa, Bwana ndiye aliyepigiwa baragumu. Mwimbieni Mungu na kupaza sauti! Mwimbieni mfalme wetu na kupaza sauti! Kwani aliye mfalme wa nchi zote ndiye Mungu, mwimbieni nyimbo zenye maana! Mungu anawatawala wamizimu nao, Mungu anakaa katika kiti chenye utakatifu wake. Wakuu wa makabila ya watu wamekusanyika, wawe ukoo wa Mungu wa Aburahamu, kwani ngao za hapa chini ni zake Mungu, ametukuka sanasana. Bwana ni mkuu na mtukufu sana, mjini mwa Mungu wetu umo mlima wenye Patakatifu pake. Ni vizuri kuvitazama, unavyoinuka huo mlima wa Sioni, nchi yote nzima huufurahia; upande wa kaskazini uko mji wa mfalme mkuu. Katika majumba yake mazuri Mungu amejulikana, ya kuwa ni ngome yenye nguvu. Tukivitazama, ni hivyo: wafalme walikula njama, wote pamoja wakaondoka kwao kupiga vita. Hapo walipouona, mara wakastuka, wakaingiwa na woga, wakakimbia. Papo hapo utetemeko ukawashika, ni uchungu kama wa mwanamke atakaye kuzaa. Kwa nguvu ya upepo wa kimbunga ukazivunja nazo merikebu zao za kwenda Tarsisi. Kama tulivyosikia, tukaviona vivyo hivyo katika mji wa Bwana Mwenye vikosi, katika mji wake Mungu wetu: Mungu ameushikiza, ukae kale na kale. Mungu, tunazikumbuka huruma zako Jumbani mwako. Kama Jina lako, Mungu, lilivyo kuu, vivyo hivyo nayo matukuzo yako yamefika mapeoni kwa nchi, mkono wako wa kuume umejaa wongofu. Mlima wa Sioni huufurahia, wana wa kike wa Yuda huyapigia vigelegele maamuzi yako. Uzungukeni mji wa Sioni na kuuzingia wote, mpate kuihesabu minara yake! Liangalieni boma lake, msilisahau mioyoni mwenu! Napo penye majumba yake piteni po pote, kusudi mvisimulie kizazi kijao, ya kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu kale na kale pasipo mwisho. Yeye hutuongoza, mpaka tutakapokufa. Makabila yote ya watu, yasikilizeni! Nyote mkaao ulimwenguni, yategeeni masikio, nyote mlio watuwatu tu, nanyi mlio mabwana! Ninyi mlio wenye mali nanyi maskini, yote pamoja! Kinywa changu kitasema yenye werevu wa kweli, nayo mawazo ya moyo wangu ni ya utambuzi. Nitaliinamisha sikio langu, lisikie mfano, nitalifumbua fumbo langu na kupiga zeze. Siku zikiwa mbaya, niogopeje, watakao kunikorofisha kinyumanyuma wakinizinga? Wao wanauegemea uwezo wao na kujivunia mali zao zilizo nyingi. Hakuna awezaye kumkomboa ndugu yake, hawezi kumpa Mungu mali za ukombozi. Kwani mali za kukomboa roho ya mtu hazilipiki, zinashindakale na kale, hazipatikani. Ijapo mtu akae sanasana, asilione kaburi, lakini hana budi kuliona, maana walio werevu wa kweli hufa, wajinga nao wasiojua kitu huangamia pamoja nao, nazo mali, walizozipata, huziachia wengine. Makaburi yao ni nyumba zao za kukaa kale na kale, ndivyo makao yao ya vizazi na vizazi, hata ikiwa wameita nchi nzima kwa majina yao. Hivyo mtu hakai na utukufu wake, hufananishwa na nyama wanaoishilizwa. Ndiko, zinakokomea njia zao waliojiegemea wenyewe, tena wanafuatwa nao waliopendezwa na maneno yao. Kama kondoo wanashurutizwa kwenda kuzimuni, mwenye kuwachunga ndiye kifo. Wanyokao mioyo watawatawala hapo patakapokucha; ndipo, ubishi wao utakapoishia, watakapokaa kuzimuni. Kweli Mungu ataikomboa roho yangu katika nguvu ya kuzimuni, naye atakayenipokea ndiye yeye. Mtu akipata mali nyingi, usihangaike, ijapo, utukufu wa nyumba yake aukuze kuwa mwingi! Kwani katika hayo yote hayamo, atakayochukua atakapokufa, utukufu wake hautamfuata kwenda kuzimuni! Akingali yupo mzima hujituliza mwenyewe, wewe nawe watu watakusifu, ukivila vyako vyenye urembo. Hivyo watu huenda kwenye kizazi cha baba zao, kusiko na mwanga kale na kale wa kuwamulikia. Mtu akiwa na utukufu wake, asiutambue, atafananishwa na nyama wanaoishilizwa. Bwana Mungu aliye Mungu kweli alisema, akaziita nchi, akianzia maawioni kwa jua, afike nako machweoni kwake. Sioni ndimo, utokeamo uzuri usiopitika, maana ndimo, Mungu atokezamo mwangaza wake. Mungu wetu anakuja, hanyamazi; moto ulao unamtangulia, upepo uvumao na nguvu unamzinga. Anaziita mbingu huko juu, hata nchi za chini, zione, jinsi atakavyowaamulia walio ukoo wake: Wakusanyeni kwangu wao wanichao, ndio waliofanya agano na mimi na kunitambikia! Ndipo, mbingu zilipoutangaza wongofu wake, kwani Mungu aliye mwamuzi ndiye yeye. Sikilizeni ninyi mlio ukoo wangu, niseme nanyi, ninyi Waisiraeli, niwashuhudie kwamba: Mungu aliye Mungu wako ndio mimi. Kwa ajili ya ng'ombe zako za tambiko sikuonyi, ng'ombe za tambiko, ulizoziteketeza, ziko machoni pangu siku zote. Sitachukua madume ya ng'ombe nyumbani mwako, wala mabeberu mazizini mwako. Kwani nyama wote wa porini ni wangu, nao wakaao milimani, ni maelfu na maelfu. Ninawajua ndege wote walioko vilimani, hata nyama walioko mashambani ni mali zangu. Kama ningekuwa na njaa, nisingesema na wewe, kwani nchi zote navyo vyote vilivyomo ni vyangu mimi. Nile nyama za ng'ombe? Au ninywe damu za mbuzi? *Kumshukuru Mungu kuwe kwako ng'ombe ya tambiko, ukimlipa yule Alioko huko juu uliyomwapia! Siku, utakaposongeka, uniite! Ndipo, nitakapokuokoa, kisha unitukuze! Lakini asiyemcha Mungu humwambia: Sababu gani unayasimulia maagizo yangu? Nacho kinywa chako kinayasemaje maneno ya Agano langu? Nawe unachukizwa unapoonywa, nayo maneno yangu unayatupia nyuma. Ukiona mwizi, ni rafiki yako, tena hufanya bia nao walio wazinzi. Kinywa chako unakisemesha yaliyo mabaya, ulimi wako hutunga madanganyo. Ukikaa na ndugu yako unamsengenya, naye mtoto wa mama yako unamtukana. Hivyo ndivyo, ulivyovifanya, nikavinyamazia; ndipo, uliponiwazia kuwa sawa kama wewe. Kwa hiyo ninakuonya nikivitolea machoni pako. Nanyi mliomsahau Mungu, yatambueni, nisije kuwararueni, pasiwepo mponya! Kunishukuru ndio ng'ombe ya tambiko initukuzayo; hiyo ni njia ya kumwonyesha mtu wokovu wa Mungu.* Nihurumie, Mungu, kwa upole wako! Kaza kuniogesha, manza, nilizozikora, zinitoke! Kusudi makosa yangu yaondoke kwangu, na unitakase! Kwani mapotovu yangu ninayajua, nayo makosa yangu ninayatazama siku zote. Wewe peke yako ndiwe, ambaye nimemkosea, nikayafanya yaliyo mabaya machoni pako; sharti wongofu wako utokezwe na maneno yako, nayo maamuzi yako yakutokeze kuwa mtakatifu. Unaona, wao, niliozaliwa nao, walikuwa wenye manza, mama yangu aliipata mimba yangu kwa kukosa. Lakini wewe unapendezwa nayo ya kweli, yakiwa ndani moyoni; unifunze, hata mambo yajifichayo yanielekee. Nieue ukininyunyizia kivumbasi, nipate kutakata! Niogeshe, nipate kung'aa kama chokaa juani! Nipe, nisikie tena shangwe za furaha, mifupa, uliyoivunja, ipige vigelegele! Ufiche uso wako, usiyaone hayo makosa yangu! Yafute manza zote, nilizozikora! Mungu, niumbie moyo utakatao! Nayo roho uirudishie upya kifuani mwangu, ipate nguvu! Usinitupe na kuniondoa usoni pako, wala Roho yako takatifu usiitoe mwangu! Nifurahishe tena na kuniokoa! Kwa kunipa roho ipendayo kutumika unishikize! Hivyo nitawafundisha wapotovu njia zako, wakosaji wapate kurudi kwako wewe! Mungu, nikomboe katika manza za damu, nilizozikora! maana u Mungu aniokoaye, ulimi wangu ukushangilie kwamba: U mwongofu! Bwana, ifumbue midomo yangu, kinywa changu kiyatangaze matukuzo yako! Kwani hupendezwi na ng'ombe za tambiko, ningekupa; nayo ng'ombe ya tambiko iteketezwayo nzima huitaki. Ng'ombe za tambiko, Mungu apendazo, ni roho ivunjikayo, moyo uliovunjika kwa kupondeka, wewe Mungu, hutaubeza. Na vikupendeze kufanya, pale Sioni pawe pazuri, nayo maboma ya Yerusalemu yajenge tena! Kisha utapendezwana ng'ombe za tambiko zilizo za kweli, ni zile za kuchomwa motoni nazo za kuteketezwa nzima; hapo ndipo, watakapokupelekea ng'ombe mezani pako pa kutambikia. Unajivuniaje ubaya, wewe jitu? Upole wake Mungu uko siku zote. Ulimi wako huwaza, jinsi utakavyoangamiza, unafanana na wembe mkali, wewe mfanya madanganyo. Unapenda mabaya kuliko mema, kuliko mambo yaongokayo unao uwongo. Unapenda maneno yote yapotezayo, kweli u mwenye ulimi wa udanganyifu. Kwa hiyo Mungu naye atakuponda, akutoweshe kale na kale, kwenye kituo chako atakupokonya, akung'oe katika nchi yao walio hai. Waongofu wakiviona wataogopa, lakini yeye watamcheka na kusema: Mtazameni mtu asiyemweka Mungu kuwa ngome yake! Aliziegemea mali zake kwa kuwa nyingi, akajivunia nguvu zake za kuangamiza watu. Lakini mimi nafanana na mchekele wenye majani mengi kwa kukaa Nyumbani mwake Mungu, kwani upole wa Mungu ndio, niliouegemea pasipo kukoma kale na kale. Nitakushukuru kale na kale kwa matendo yako, nitalingojea Jina lako lipendezalo kwao wakuchao. Mpumbavu husema moyoni mwake: Hakuna Mungu. Hawafai kitu, mapotovu yao hutapisha, anayefanya mema hayuko huko. Mungu huchungulia toka mbinguni, awatazame wana wa watu, aone, kama yuko mwenye akili anayemtafuta Mungu. Lakini wote pamoja walirudi nyuma, wote ni waovu, hakuna anayefanya mema, hakuna hata mmoja. Je? Wale wote wafanyao maovu hawataki kujitambua, wao wanaowala walio ukoo wangu, kama walavyo mkate? Lakini Mungu hawamtambikii! Patafika, watakapotetemeka kwa kustuka mastuko yasiyokuwa bado, kwa kuwa Mungu ataitapanya mifupa yao waliokuvizia, kwa kuwa Mungu atakuwa amewatupa, atawatia soni. Laiti wokovu wake Isiraeli utokee Sioni, Mungu awarudishe mateka walio wa ukoo wake! Ndipo, Yakobo atakaposhangilia, ndipo, Isiraeli atakapofurahi. Mungu, kwa ajili ya Jina lako niokoe! Kwa nguvu zako kuu niamulie! Mungu, maombo yangu yasikie na kuyasikiliza maneno ya kinywa changu! Kwani wasio wa kwetu wameniinukia, wanaitafuta roho yangu wao wakorofi, lakini yeye aliye Mungu hawamtazami. Ninajua: Mungu ndiye anayenisaidia, ndiye anayeishikiza roho yangu. Uwarudishie ubaya wao waninyatiao! Kwa maana u mkweli uwamalize! Kisha nitakutolea ng'ombe za tambiko kwa kupendezwa, nitalishukuru Jina lako kuwa lenye wema. Kwani katika masongano yote umeniopoa, macho yangu yakapata kuwafurahia wachukivu wangu. Kwa mwimbishaji. Fundisho la Dawidi la kuimbia mazeze. Sikiliza Mungu, kuomba kwangu! Usijifiche, nikikulalamikia! Niangalie, uniitikie! Ninahangaika kwa kulia kwangu na kupiga kite. Kwa sababu adui wananizomea, nao wasiomcha Mungu wananisonga, kwani wanataka, mateso yaniangukie, kwa ukali tu wananipingia. Moyo wangu humu ndani yangu unatetemeka, mastuko kama ya kufa yakaniguia; masukosuko ya mwili yananijia kwa kuogopa tu, nikapigwa sana na bumbuazi. Nikasema: Ningepata mabawa kama ya njiwa, ningeruka na kutua pawapo pote! Mara wangeniona, nikienda mbali, nikae nyikani. Ningepiga mbio kulifikia kimbilio langu, niondoke kwenye upepo uvumao na nguvu kama za kimbunga. Waangamize Bwana, ukiwavuruga, wapitane wanaposema, kwani mjini mimeona makorofi na magomvi. Mchana kutwa na usiku kucha huzungukia kwenye maboma yake, lakini mjini mna mapotovu na maumivu. Mle mjini mnaangamika, unyang'anyi na udanganyifu hauondoki katika mitaa yake. Tena anayenitukana siye adui yangu, ningevumilia, wala siye mchukivu wangu anayejikuza, aninyenyekeze; kama ndiye, ningejificha, asinione. Ila ndiwe wewe mwenzangu, ambaye tuliliana damu, tena ulikuwa mwenyeji wangu mimi. Vilikuwa vyenye utamu, jinsi tulivyoendeleana, tulivyokwenda pamoja na makundi ya watu Nyumbani kwake Mungu. Kifo na kiwakamate, washuke kuzimuni wakingali wa hai! Kwani katika makao yao na katika mioyo yao yamo mabaya tu. Mimi ninamlilia Mungu, yeye Bwana ataniokoa. Jioni na mapema na mchana kutwa na nilalamike na kupiga kite; ndipo, atakapoisikia sauti yangu. Ataikomboa roho yangu, nikae na kutengemana, wao wasinifikie, ijapo wawe wengi wanaonijia; Mungu husikia, naye atawajibu. Yeye ndiye akaaye tangu kale. Wao hawataki kugeuka, kwa kuwa hawamwogopi aliye Mungu. Maana wanawakamata nao waliomkalia Mungu, nalo Agano lake wanalipinga. Wayasemayo ni mafuta ya midomo, ni matamu kuliko maziwa, lakini mioyoni mwao huwaza vita. Maneno yao, wayasemayo, hulegea kuliko mafuta ya uto, lakini wenyewe ndio panga zilizokwisha kuchomolewa. Umtupie bwana yakulemeayo! Yeye atakumalizia, hatamtoa mwongofu, atikisike kale na kale. Nawe Mungu, uwatelemshe, waje shimoni mwenye kuoza! Wale wenye manza za damu na madanganyo siku zao hawatazifikisha kati, lakini mimi ninakuegemea. Kwa kuwa wako watu wanaonifokea, nihurumie Mungu! Siku zote wananigombeza na kunitesa. Hao wanaonisonga wananifokea siku zote, kwani ni wengi wanaonigombeza kwa majivuno tu. Siku, ninaposhikwa na woga, ninakuegemea wewe. Kwa kuwa naye Mungu na nilitukuze Neno lake, kwa kumwegemea Mungu sitaogopa kamwe; wenye miili ya kimtu wanifanyieje? Siku zote huyabishia maneno yangu, waniumize, kwa mawazo yao yote hunitafutia mabaya. Wao hujikusanya, waniotee na kupanyatia, nyayo zangu zilipo, kwa sababu wanangojea kuipata roho yangu. Kwa ajili ya mapotovu yao hawataona wokovu, watu walio hivyo uwachafukie, Mungu, na kuwakumba! Siku za kutangatanga kwangu umezihesabu wewe, machozi yangu nayo yakusanye kwako katika kichupa! Najua, yamo katika kitabu chako, umeyaandika. Hapo, watakaporudi nyuma adui zangu, itakuwa siku ile, nitakapokuitia; maana hili ninalijua, ya kuwa Mungu yuko upande wangu. Kwa kuwa naye Mungu na nilitukuze Neno lake, kwa kuwa naye Bwana na nilitukuze Neno lake. Kwa kumwegemea Mungu sitaogopa kamwe; walio watuwatu tu wanifanyieje? Niliyokuapia, Mungu, nitakulipa, nikushukuru. Kwani umeiopoa roho yangu katika kufa; kweli, hata miguu yangu unaiangalia, isijikwae, ipate kuendelea machoni pa Mungu penye mwanga wao wenye uzima. Nihurumie, Mungu! Nihurumie! Kwani roho yangu imekukimbilia wewe, kivuli kilichoko mabawani kwako nimekikimbilia, mpaka yaishe kupita mateso haya. Ninamwita Mungu alioko huko juu, ni yeye Mungu atakayenimalizia mashauri yangu. Atamtuma toka mbinguni atakayeniokoa, naye anifokeaye atamtia soni. Mungu hutuma upole wake nao welekevu wake. Hapa, roho yangu ilipotua, ni penye simba, nao wanipuliziao pumzi za moto ni wana wa watu, mikuki na mishale ni meno yao, nazo ndimi zao ndio panga zenye ukali. Utukuke, Mungu, juu mbinguni, nazo nchi zote ziuone utukufu wako! Miguu yangu waliitegea matanzi, nayo roho yangu wanaiinamiza. Walinichimbia mwina mimi, wakatumbukia humo. E Mungu, moyo wangu umetulia na kushupaa, moyo wangu umetulia kweli na kushupaa; kwa hiyo na niimbe na kupiga shangwe! Amka, roho yangu yenye matukuzo! Amkeni, pango na zeze, niiamshe mionzi ya jua! Kwenye makundi ya watu wako nitakushukuru, Bwana, nako kwenye wamizimu nitakuimbia. Kwani upole wako ni mkubwa, unafika mpaka mbinguni, nako mawinguni unafika welekevu wako. Utukuke, Mungu, juu mbinguni, nazo nchi zote ziuone utukufu wako! Ni vya kweli hivyo, mnavyohukumu, ninyi wakuu? nayo maamuzi yenu yananyoka, ninyi wana wa watu? Sivyo! Kwani mioyoni mwenu yamo mapotovu; ndiyo mnayoyafanya, nayo makorofi ya mikono yenu mnayaendesha katika nchi. Wasiomcha Mungu hukataa kutii tangu kuzaliwa kwao, wasemao uwongo hupotea hivyo, walivyozaliwa. Sumu inayofanana na sumu ya nyoka wao wanayo, wafanana na pili asiyesikia kwa kuyaziba masikio, ni yule asiyesikiliza sauti ya mganga, ijapo ajue sana kufinga nyoka kwa huo uganga. Mungu yavunje meno yao vinywani mwao! Nayo magego ya wana wa simba yang'oe, Bwana! Sharti wakauke kama maji yanayojiendea tu, mishale yao sharti iwe, kama haina chembe, watakapoielekeza! Wawe kama kovya linalokwenda na kuyeyuka, au kama mimba ya mwanamke iharibikayo pasipo kuona jua. Hivyo nayo miiba yenu ikiwa haijakomaa penye miti yao, ataipeperusha kwa ukali wa moto, ijapo iwe mibichi! Mwongofu atafurahi akiyaona malipizi hayo, ataiogesha miguu yake katika damu yake asiyemcha Mungu. Ndipo, watu watakaposema: kumbe mwongofu hupata! Kumbe yuko Mungu ahukumuye katika nchi! Niopoe, Mungu wangu, mikononi mwao walio adui zangu, ukinikingia walioniinukia, wasinifikie! Niopoe mikononi mwao wafanyao mapotovu! Niokoe mikononi mwao wauao wenzao! Kwani unaona, jinsi wanavyoivizia roho yangu, wenye nguvu wamekusanyika, wanikamate; lakini hakuna, Bwana, nilichowapotolea, wala nilichowakosea. Kweli hakuna mabaya, niliyowafanyizia, tena wanapiga mbio, wajiweke tayari. Amka, unifikie, uwaone! Nawe Bwana Mungu, uliye Mwenye vikosi, uliye Mungu wa Isiraeli, inuka, uwapatilize wamizimu wote! Usiwahurumie hata mmoja wao waliokuacha kwa upotovu tu! Jioni hurudi na kulia kama mbwa; ndivyo, wanavyozungukazunguka humu mjini. Ukiwaangalia, vinywani mwao hububujika mabaya, namo midomoni mwao zimo panga; huwaza kwamba: Yuko nani atakayetusikia? Lakini wewe Bwana, unawacheka, wamizimu wote unawabeza. Wakikaza nguvu, nitakutazamia wewe; kwani wewe, Mungu, u ngome yangu. Mungu wangu aliye mwenye upole hunijia mbele, yeye Mungu hunipa kuwashangilia wao walionisonga. Kusudi walio ukoo wangu wasivisahau, usiwaue kabisa! Wapoteze tu kwa nguvu yako, waje kutangatanga! Kisha uwakumbe, waje kuzimuni! Wewe Bwana, u ngao yangu. Vinywa vyao hukosa, midomo yao inaposema, sharti wanaswe na majivuno yao wakizidi kuapiza na kuogopa! Waishilize kwa kuwachafukia! Waishilize, watoweke! Hivyo ndivyo, yatakavyojulikana nako mapeoni kwa nchi, ya kuwa Mungu ndiye awatawalaye wa Yakobo. Jioni hurudi na kulia, kama ni mbwa; ndivyo, wanavyozungukazunguka humu mjini. Wao sharti waje kutangatanga na kutafuta chakula, kisha sharti walale pasipo kushiba! Ndipo, mimi nitakapoziimbia nguvu zako, asubuhi nitaushangilia upole wako, kwani umekuwa ngome yangu na kimbilio langu hapo, niliposongeka. Wewe uliye nguvu zangu, nitakuimbia, kwani wewe, Mungu, u ngome yangu, u Mungu wangu mwenye upole. Mungu, umetutupa na kututapanya; kweli ulikuwa umetuchafukia, lakini utugeukie! Umeitetemesha nchi na kuipasua, sasa ziponye nyufa zake, maana imetingishika. Walio ukoo wako umewaonea magumu, ukatunywesha mvinyo za kutupepesusha. Lakini wao wakuogopao umewapa bendera ya kuinuliana, wapate kuyagombea yaliyo ya kweli. Kusudi wao uwapendao wapate kuopoka, mkono wako wa kuume uwaokoe, ukituitikia! Mungu alisema hapo Patakatifu pake: Nikiigawanya nchi ya Sikemu nitapiga vigelegele; ndipo, nitakapolipima nalo bonde la Sukoti. Gileadi ni yangu, Manase ni yangu, Efuraimu ni kingio la kichwa changu, Yuda ni bakora yangu ya kifalme. Moabu ni bakuli langu la kunawia, Edomu ndiko, nitakakovitupia viatu vyangu, nchi ya Wafilisti itanishangilia. Yuko nani atakayenipeleka mjini mwenye maboma? Yuko nani atakayeniongoza mpaka Edomu? Si wewe Mungu uliyenitupa, ukakataa kwenda vitani na vikosi vyetu? Tujie, utusaidie, tumshinde atusongaye! Kwani watu hawawezi kutuokoa. Kwa nguvu yake Mungu na tufanye nasi yenye nguvu! Yeye ndiye atakayewakanyaga watusongao. Mungu, lisikie lalamiko langu! Yaitikie nikuombayo! Kwenye mapeo ya nchi ninakuita, moyo wangu ukizimia. Unikweze mwambani! Kwani ni mrefu wa kunishinda. Kwani kimbilio langu ndiwe wewe, u mnara wenye nguvu machoni pao adui. Ninataka kuwamo katika kituo chako kale na kale, na kulikimbilia ficho lililomo mabawani mwako. Kwani wewe, Mungu, umeyasikia niliyokuapia, ukanigawia fungu lao waliogopao Jina lako. Unamwongezea mfalme siku kwa siku, miaka yake iwe ya vizazi na vizazi. Akiendelea machoni pake Mungu atakaa kale na kale. Agiza vya upole na vya kweli, vimsimamie! Hivyo nitaliimbia Jina lako kale na kale na kuyalipa siku kwa siku niliyokuapia. Roho yangu inamnyamazia Mungu peke yake, wokovu wangu utoke kwake yeye. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, ndiye ngome yangu, sitatikisika kamwe. Mpaka lini ninyi nyote mwamrukia mtu mmoja, mpate kumwua? mpaka awe kama ukuta unaoyumbayumba au kama kitalu kichakaacho? Njama zao ni kutafuta, jinsi watakavyomwondoa katika ujumbe, kwa hiyo hupendezwa na uwongo. Vinywa vyao hubariki, lakini mioyoni wanaapiza. Roho yangu, umnyamazie Mungu peke yake! Kwani kwake yeye ndiko, kingojeo changu kiliko. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, ndiye ngome yangu, sitatikisika. Wokovu wangu na utukufu wangu uliko, ndiko kwake Mungu, ni mwamba wangu wenye nguvu, kimbilio languliko kwake Mungu. Mwegemeeni siku zote, ninyi wenzangu wa ukoo! Imimineni mioyo yanu mbele yake! Kimbilio letu ndiye Mungu. Kweli wana wa watu huwa mvuke, nao ubwana wao ni wa uwongo; wakipimwa katika mizani, hupanda juu, wote pamoja ni wepesi kuliko mvuke. Msiuegemee ukorofi wala unyang'anyi, usiwapofushe! Mali zikiwa nyingi, msiziweke mioyoni! Mungu alisema neno moja, nimelisikia mara mbili zote, ni lile la kwamba: Nguvu ni yake Mungu. Wewe Bwana u mwenye upole, utamlipa mtu, kama matendo ya mtu yalivyo, ndivyo, utakavyomlipa. Mungu, wewe u Mungu wangu, ninakutafuta mapema; roho yangu ina kiu ya kunywea kwako, nazo nyama za mwili wangu zinakutunukia sana, hapa katika nchi kavu ichokeshayo kwa kuwa pasipo maji. Hivyo ndivyo, nilivyokutazamia Patakatifu pako, niione nguvu yako na utukufu wako. Kwani upole wako ni mwema kuliko uzima; kwa hiyo midomo yangu sharti ikusifu. Hivyo nitakutukuza siku zangu zote, nitakazokuwapo, Jina lako nitaliinulia mikono yangu. Hivi vinaishibisha roho yangu kama kiini cha mafuta, midomo yangu ikikupigia vigelegele, kinywa changu kikikushangilia. Ninapokwenda kulala ninakukumbuka, napo ninapoamka ninayawaza mambo yako. Kwani wewe ndiwe uliyenisaidia, namo kivulini mwa mabawa yako ninapiga shangwe. Roho yangu inagandamana nawe wewe, mkono wako wa kuume ukanishikiza. Lakini wao wanaoitafuta roho yangu, waiangamize, sharti washuke kuzimuni huko ndani ya nchi. Watu watawatoa, wauawe kwa ukali wa panga, kisha watakuwa chakula chao mbwa wa mwitu. Lakini mfalme atafurahia kuwa wake Mungu, wote wamwapiao yeye watashangilia, kwani vinywa vyao wasemao uwongo vitafumbwa. Mungu, isikie sauti yangu, nikikulalamikia! Unilinde, nikae na kutengemana, mchukivu akinitisha! Unifiche, njama zao wafanyao mabaya zisinijie, wala fujo yao wafanyao mapotovu! Ndimi zao wamezinoa, ziwe zenye ukali kama wa upanga, mishale yao, wanayotaka kuipiga, ni maneno machungu. Hujificha, wapate kumpiga mishale amchaye Mungu, mara wanampiga, kisha hawaogopi. Hushikana mioyo, wazidishe ubaya, maongezi yao ni hayo tu, jinsi watakavyotega matanzi. Yuko nani atakayeyaona? ndivyo, wanavyosema. Huwaza makorofi kwa kusema: Tumeijua mizungu yote. Yaliyomo mioyoni mwao kila mmoja hayachunguziki. Lakini Mungu atakapowapiga mishale, mara watakuwa wameumia. Ndimi zao ndizo zilizowaangusha, wote watakaowaona hivyo watawasimanga. Ndipo, watu wote watakapoogopa, wataungama kwamba: Ni kazi ya Mungu! Ndivyo, watakavyoyatambua matendo yake. Hapo mwongofu atafurahia kuwa wa Bwana, amkimbilie, nao wote wenye mioyo inyokayo watashangilia. Mungu, ukitukuzwa mle Sioni, huwamo kimya, wewe ndiwe unayelipwa, watu waliyokuapia. Unawasikia wao wanaokuomba, kwa hiyo wenye miili ya kimtu hukujia wote. Manza, tulizozikora, zinatulemea, lakini wewe unayafunika nayo mapotovu yetu. Mwenye shangwe ni mtu, uliyemchagua, ukamkaribisha kukaa uani kwako. Ndipo, tunaposhibishwa mema ya Nyumba yako, ni kwamba: ya Kao lako lililo takatifu. Kwa wongofu wako unaotisha unatuitikia, wewe Mungu uliyetuokoa. U egemeo lao wote wakaao nchini hata mapeoni kwake, nalo lao wakaao mbali huko baharini. Uliishikiza milima kwa uwezo wako, ukajifunga nguvu zishindazo zote. Unautuliza uvumi wa bahari, hata uvumi wa mawimbi, nayo machafuko yao makabila ya watu. Kwa hiyo wakaao mapeoni kwa nchi huviogopa vielekezo vyako, nawe unawafurahisha wakaao maawioni nako machweoni kwa jua. Umeitokea nchi, ukainywesha, ukaichipuza sanasana, mto wake Mungu hujaa maji, ukawavunisha watu vilaji vingi, kwani hivyo ndivyo, unavyoiotesha nchi: matuta yake huyanywesha vizuri, mashamba yapate kulowana, mvua nyingi zikiyalegeza; ndivyo, unavyoibariki hiyo mimea yake. Magawio yako mema ya kilimo ni kama kilemba cha mwaka, nazo nyayo zako zinadondosha mafuta. Mbuga za nyika zimechipuka, nazo zinadondoka, vilima navyo vimejitega kushangilia. Nyanda zimejaa kondoo, mabonde yamefunikwa na mashamba, nao watu wanapigiana shangwe nazo nyimbo. Mpigieni Mungu shangwe, ninyi nchi zote! Uimbieni utukufu wa Jina lake! Mtukuzeni na kumsifu! Mwambieni Mungu: Kweli matendo yako ndiyo yanayostaajabisha, kwa nguvu zako nyingi watakunyenyekea nao wachukivu wako. Nchi zilizoko zote zinakuangukia, wanakuimbia wewe, nalo Jina lako wanaliimbia. Njoni, mvione vioja vya Mungu! Jinsi anavyowaendea wana wa watu, ni vya kustaajabu. Bahari aliigeuza kuwa nchi kavu, wakapita kwa miguu kwenye mto mkubwa; kwa hiyo tunamfurahia aliye hivyo. Hutawala kwa uwezo wake mkubwa kale na kale, macho yake huyatazama makabila ya watu, waliomwacha hawatajivuna mbele yake. Ninyi makabila ya watu, mtukuzeni Mungu wetu! Pazeni sauti za kumsifu! Roho zetu huzipa kuwa zenye uzima, haiachi miguu yetu, ujikwae. Kweli ulitujaribu, Mungu, na kutuyeyusha, kama ni fedha, watu wanazoziyeyusha, ukatupeleka kifungoni na kututwika mzigo uliotulemea viunoni, ukaleta watu, watukanyage vichwa, tukaingia motoni namo majini, lakini ulitutoa mle, ukatukalisha panapo mema mengi. Nitakuja, nikupelekee ng'ombe za tambiko Nyumbani mwako, nikulipe hayo, niliyokuapia, midomo yangu ilipofumbuka kwa hivyo, nilivyokuwa nimesongeka; ilikuwa hapo, kilipoyasema kinywa changu. Nitakupelekea ng'ombe za tambiko zenye mafuta pamoja na nyama za kondoo za vukizo; kweli ni ng'ombe na kondoo, nitakaokutengenezea. Njoni, msikilize, nyote mmwogopao Mungu, niwasimulie aliyoifanyizia roho yangu. Nilikifumbua kinywa changu, nikamlalamikia, tena ulimi wangu nao ulikuwa umejitega, upate kumtukuza. Kama ningalikuwa nimeuelekeza moyo wangu kwenye maovu, Bwana angalikataa kunisikia. Neno hili ni la kweli: Mungu husikia; akaisikiliza nayo sauti ya lalamiko langu. Mungu na atukuzwe, maana hakuninyima niliyomwomba, wala hakuninyima upole wake. Mungu na atuhurumie atubariki! Auangaze uso wake, atumulikie! Tupe, tuitambue njia yako katika nchi, tuone kwa mataifa yote, jinsi unavyookoa! Na yakushukuru, Mungu, makabila ya watu, kweli wao wa makabila yote ya watu na wakushukuru. Makabila yote ya yafurahi na kushangilia, kwani unayaamulia makabila ya watu kwa wongofu, makabila yaliyoko katika nchi huyaongoza. Na yakushukuru, Mungu, makabila ya watu, kweli wao wa makabila yote ya watu na wakushukuru. Nchi ikiyaotesha vema mazao yake, Mungu aliye Mungu wetu hutubariki. Mungu hutubariki, wamwogope wote walioko huku nchini hata mapeoni kwake. Mungu akiinuka, hutawanyika walio adui zake, nao wamchukiao hukimbia machoni pake! Kama moshi unavyopeperuka, ndivyo, wanavyopeperuka; kama nta inavyoyeyuka motoni, ndivyo, wanavyoangamia usoni pake Mungu wao wasiomcha. Lakini waongofu hufurahi na kushangilia kwa kuchangamka na kuona furaha mbele ya Mungu. Mwimbieni Mungu, nalo Jina lake lishangilieni! Mtengenezeeni njia apitaye nyikani! Bwana ni Jina lake, mpigieni vigelegele! Ni baba yao wafiwao na wazazi, nao wajane huwaamulia, ni Mungu akaaye pake, napo ni patakatifu. Ni Mungu apaye wakiwa nyumba za kukaa, hutoa wafungwa kifungoni, nao wafanikiwe, lakini kwao wabishi, watakakokaa, ndiko kukavu. Mungu, hapo, ulipotoka kuwatangulia wao walio ukoo wako, napo hapo, ulipokwenda kukanyaga kwenye jangwa, ndipo, nchi ilipotetemeka, nazo mbingu zikanyesha maji, Mungu huyu alipotokea kule Sinai, alipotokea yeye Mungu aliye Mungu wao Waisiraeli. Mvua ifurikayo ukiinyesha, Mungu, ilikuwa kila mara, fungu lako lilipotaka kuzimia; ndivyo, wewe ulivyolishikiza. Walio kundi lako wakapata pa kukaa, nao wanyonge ukawashikiza, Mungu, kwa wema wako. Wenye kulitangaza neno, alilolitoa bwana, ni kikosi kikubwa. Wafalme wa vikosi watakimbia, watakimbia kweli, nao wanawake wenye nyumba watagawanya mateka. Hapo, mnapolala kambini, yapo yanayomerimeta, yanafanana na mabawa ya kwenzi yang'aayo kama fedha, nayo manyoya yake humetuka kama dhahabu. Mwenyezi alipowatawanya wafalme wale, mara kuling'aa kama theluji kulikokuwa na giza kuu. Mlima wake Mungu ni mlima wa Basani, ule mlima wa Basani ulio wenye vilima huko kileleni. Ninyi milima yenye vilima kileleni juu, sababu gani mnautazama kwa kijicho mlima ule Mungu alioupenda, akae pale? Kweli Bwana atakaa pale kale na kale Magari yake Mungu ni maelfu na maelfu, hayahesabiki, Bwana anayo kule Sinai kwenye Patakatifu pake. Ulipopaa juu, uliteka mateka, nako kwa watu ukayapokea waliyokupa; hata wabishi hawana budi kukaa kwake Bwana Mungu. Bwana na atukuzwe siku kwa siku! Mungu hututwika mzigo, lakini hutusaidia kuuchukua. Mungu, tuliye naye, ndiye Mungu aokoaye, mwenye njia za kutoka nako kufani ni Mungu Bwana. Lakini vichwa vyao wachukivu wake Mungu ataviponda, nazo tosi zao wafulizao kukora manza zitachujuka. Bwana alisema: Nitawatoa kule Basani, niwarudishe, nitawatoa namo vilindini mwa bahari, niwarudishe. Ndipo, utakapoiogesha miguu yako katika damu, nazo ndimi za mbwa wako zitapata mafungu yao kwa adui zako. Watu huwatazama wanaokuendea, Mungu, wakimwendea patakatifu aliye Mungu wangu hata mfalme wangu. Waimbaji wanakwenda mbele, wapiga mazeze huwafuata, katikati ni wanawali wapigao patu. Mnapokusanyika mtukuzeni Mungu Bwana, ninyi mnywao maji kisimani kwao Waisiraeli! Wako wa Benyamini aliye mdogo, tena huwatawala, wako wakuu wa Yuda walio vikosi vizima, wako wakuu wa Zebuluni, nao wa Nafutali! Mungu wako ameviagiza vitakavyokupa nguvu; Mungu, ufulize kuyatia nguvu uliyotufanyizia! Kwa ajili ya Nyumba yako iliyo ya kutambika sharti wafalme wakupelekee matunzo huko Yerusalemu. karipia nyama wakaao bwawani! ndio wakorofi wote, huwa ng'ombe wakali wanaowakanyaga ndama, kwani ni fedha tu, wanazozitamani. Nayo makabila ya watu wapendao vita yatapanye kabisa! Ndipo, wakuu wa Misri watakapotokea, nao watu weusi, ndio watakaoviinua mikono yao kumwelekea Mungu. Mwimbieni Mungu, ninyi wafalme wa nchi, pamoja wa watu! Mshangilieni aliye Bwana! Ni yeye akaliaye mbingu zilizoko kule juu, nazo ni za kale, ni yeye avumishaye sauti yake, ikinguruma na nguvu. Mkuzeni Mungu kuwa mwenye nguvu! Waisiraeli ndio, uliowatokea utukufu wake, nguvu zake ziko juu mawinguni. Mungu, unaogopesha toka Patakatifu pako, Mungu wa Isiraeli; yeye ndiye atakayeupa ukoo wake nguvu za kushupaa. Na atukuzwe yeye Mungu! Na uniokoe, wewe Mungu! Kwani yamekuja maji ya kuipata roho yangu. Ninazama bwawani pabonyekapo, nisione pa kusimama, nimeingia katika vilindi vya maji, mkondo wao ukanididimiza. Nikachoka kwa kupiga kelele, mmeo ukakauka, nikizidi kumtazamia Mungu wangu, macho yakanizimia. Wanaonichukia bure ni wengi kuliko nywele za kichwani pangu, adui zangu watakao kunimaliza kwa kunionea wamepata nguvu, nashurutishwa kuyarudisha nisiyoyapokonya. Wewe Mungu unaujua upumbavu wangu, nazo manza, nilizozikora, hazikufichika kwako. Usiache, kwa ajili yangu mimi wapatwe na soni wakungojeao wewe, Bwana Mungu Mwenye vikosi! Kwa ajili yangu mimi wasisimangike wakutafutao wewe, Mungu wa Isiraeli! Kwani ni kwa ajili yako wewe, nikivumilia mabezo, ijapo soni ije kuufunika uso wangu. Nimekwisha kuwa mgeni kwao ndugu zangu, watoto wa mama yangu hawanijui, kama si mtu wa kwao. Kwani kwa ajili ya Nyumba yako wivu unanila, nayo masimango yao wanaokusimanga yameniguia mimi. Nikalia pamoja na kujiumiza kwa kufunga, lakini wao wananisimangia navyo hivyo. Nikatumia gunia kuwa vazi langu, nikawa kwao kama fumbo. Wanaokaa langoni hunicheka, nao walevi hupiga mazeze ya kunifyoza. Lakini mimi ninakulalamikia, Bwana, mpaka utakapopendezwa. Mungu, kwa upole wako mwingi uniitikie na kunionyesha welekevu wako nao wokovu wako! Nitoe kwenye matope, nipate kusimama, niokoke mikononi mwao wanichukiao namo vilindini mwa maji! Mkondo wa maji usinididimize, wala bwawa lisinimeze! wala kisima kisinifungie njia ya kutoka! Bwana, kwa upole wako ufanyao mema na uniitikie! Kwa kunionea uchungu mwingi na unigeukie! Usimfiche mtumishi wako uso wako! Kwani nimesongeka, usikawe kuniitikia! Ifikie roho yangu karibu, uikomboe! Kwa ajili ya wachukivu wangu niokoe! Wewe unayajua matusi na matwezo na masimango yaliyonipata, mbele yako wewe wako wote wanisongao. Hivyo, ninavyotukanwa vimenivunja moyo, hata nikaugua; nikangoja, kama yuko mwenye huruma, lakini hakuna; nikangoja, kama yuko mtuliza moyo, lakini sikumwona. Kilaji, walichonipa, ni maji ya nyongo, napo, nilipopatwa na kiu, walininywesha siki. Sharti meza zao ziwawie matanzi, walipizwe mabaya yao wakinaswa nayo! Macho yao sharti uyafanya kuwa giza, wasione kabisa, viuno vyao sharti uvitetemeshe siku zao zote! Yamwage makali yako, yawapate, nao moto wa machafuko yako sharti uwafikie! Sharti mahame tu yawe pao pa kukaa, asioneke atakayekaa hapo, walipotua! Kwani uliyempiga wewe, wanamkimbiza, nayo maumivu yao, uliowaumiza, wanayasimuliana. Waache, wajiongezee manza kwa manza, wasije kufika hapo, wongofu wako ulipo! Sharti wafutwe katika kitabu chao walio wenye uzima, wasiandikwe pamoja nao walio waongofu! Lakini mimi ni mkiwa mwenye maumivu, wokovu wako, Mungu, ndio utakaonitia nguvu. Nitalitukuza Jina la Mungu na kuliimbia, kwa kumshukuru nitamkuza. Hivi vitampendeza Bwana kuliko ng'ombe, ijapo awe dume lenye pembe na kwato kubwa. Maskini wakiviona watafurahi, nayo mioyo yenu ninyi mnaomtafuta Mungu na irudishwe uzimani. Kwani Bwana huwasikia wasio na mali, nao walio wake wakifungwa, hawabezi. Mbingu na nchi na zimtukuze, nazo bahari navyo vyote vinavyotembea humo! Kwani Mungu atauokoa Sioni atakapoijenga miji ya Yuda, watu wakae humo na kuitunza! Navyo vizazi vya watumishi wake vitaitwaa, nao walipendao Jina lake watakaa humo. Mungu, piga mbio, uniopoe! Bwana, pigambio, unisaidie! Sharti wapatwe na soni wakiumbuliwa walioitafuta roho yangu. Sharti warudishwe nyuma na kutwezwa wao waliopendezwa na mabaya yaliyonipata mimi. Sharti warudi nyuma na kuona soni wale walioniambia: Weye! Weye! Sharti wachangamke na kufurahiwa wote wakutafutao! Waupendao wokovu wako waseme pasipo kukoma: Mkuu ni Mungu! Nami mnyonge, hata mkiwa; Mungu, piga mbio, unijie! Msaada wangu na wokovu wangu ndiwe wewe; wewe Bwana, usinikawilie! Wewe Bwana, nimekukimbilia, sitapatwa na soni kale na kale. Kwa kuwa u mwongofu, niopoe na kuniponya! Nitegee sikio lako, ukaniokoe! Niwie mwamba wenye nguvu, niujie siku zote, maana uliniagia, ya kuwa utaniokoa. Kwani mwamba wangu na boma langu ndiwe wewe. Mungu wangu, niponye mikononi mwao wasiokucha! Namo mikononi mwao wapotovu namo mwao wakorofi! Kwani wewe Bwana Mungu, u kingojeo changu, u kimbilio langu tangu hapo, nilipokuwa mtoto. Nimejishikiza kwako tangu hapo, nilipozaliwa, wewe ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu; ninakushangilia siku zote. Kwao wengi ni kama kielekezo, wakiniona, nawe ndiwe kimbilio langu lenye nguvu. Kinywa changu kinazidi kukushangilia, siku zote huutangaza utukufu wako. Siku, nitakapokuwa mzee, usinitupe, nguvu yangu itakapoishia, usiniache! Kwani wachukivu wangu wamekwisha kusema, nao wanaoingoja roho yangu wamekula njama pamoja: Mungu amemwacha; mkimbizeni, mmkamate! Kwani hakuna tena atakayemwopoa. Wewe Mungu, usiniendee mbali! Mungu wangu, piga mbio, unisaidie! Sharti wapatwe na soni, sharti waangamie wao waliotakia mabaya roho yangu. Sharti wajifunike kwa kutwezwa wakiumbuka waliotafuta mabaya ya kunifanyizia. Lakini mimi nitangoja siku zote pamoja na kufuliza kukupigia shangwe vivyo hivyo. Kinywa changu kitayasimulia mambo ya wongofu wako na kuutangaza wokovu wako siku zote, kwani sijui kuyahesabu, kama ni mangapi. Ninaendelea bado kwa nguvu za Bwana Mungu zilizo kuu, ninayowakumbusha si mengine, ni wongofu wako tu. Mungu, ulinifundisha tangu hapo, nilipokuwa mtoto; kwa hiyo ninayatangaza mataajabu yako. Sasa napo hapo, nitakapokuwa mzee mwenye mvi, usiniache, Mungu, niwatangazie vizazi vingi kazi za mkono wako nayo matendo yako yenye nguvu kwao wote watakaokuwapo. Wongofu wako, Mungu, unakua kufika hata mbinguni, wewe ndiwe ufanyaye mambo makuu. Mungu, afananaye na wewe yuko nani? Wewe ulipotuacha, tuliona masongano mengi na mabaya; lakini utaturudisha tena, utupatie uzima, utatutoa huko ndani ya nchi, utuweke juu yake. Ukuu, utakaonipa, utazidi, utakaponigeukia, unitulize moyo. Nami nitakushukuru na kukupigia pango kwa welekevu wako, Mungu wangu, nitakuimbia na kupiga zeze, wewe Mtakatifu wa Isiraeli. Midomo yangu inashangilia, kwa hiyo ninakuimbia, roho yangu inashangilia nayo, kwa maana umeikomboa. Nao ulimi wangu unausimulia wongofu wako mchana kutwa, kwani waliotafuta mabaya ya kunifanyizia huiva nyuso kwa soni. Mungu, mpe mfalme kuamua, kama unavyoamua! Naye mwana wa mfalme mpe wongofu ulio kama wako! Awahukumu walio ukoo wako kwa wongofu, nayo mashauri yao wanyonge wako ayanyoshe! Milima iwe yenye matengemano ya kuwagawia watu, navyo vilima vilevile kwa nguvu ya wongofu! Walio wanyonge kwao atawaamulia, nao wana wao maskini atawaokoa, lakini wakorofi atawaponda. Jua likingali liko, watakuogopa wao wavizazi na vizazi, mwezi utakavyoviwakia. Atashuka kama mvua inyweshayo uchome, au kama manyunyu ya mvua yalegazayo nchi. Mwongofu atachipuka siku, atakazokuwapo; mpaka mwezi utakapokuwa hauko tena, utengemano utazidi. Atatawala, bahari inakoanzia, mpaka huko, inakoishia, tena kuanzia kwenye jito kubwa mpaka mapeoni kwa nchi. Wakaao nyikani watampigia magoti, sharti walambe mavumbi walio adui zake. Wafalme wa Tarsisi na wa visiwa watampelekea matunzo, nao wafalme wa Arabia na wa Saba wataleta mahongo. Wafalme wote pia watamwangukia, nao wamizimu wote watamtumikia. Kwani atamwopoa maskini amliliaye, hata mnyonge akosaye mwenye kumsaidia. Atamhurumia akorofikaye naye mkiwa, aziokoe roho zao walio wakiwa. Atazikomboa roho zao mwao wanyang'anyi namo mwao wakorofi, maana damu zao ni zenye kiasi kikubwa machoni pake. Na akae akiwa mwenye uzima, wamgawie nazo dhahabu za Arabia! Na wamwombee pasipo kukoma, wamtukuze siku zote. Vilaji vifurike katika nchi mpaka juu milimani! Miti yake ya matunda na ivume kama miti ya Libanoni! Namo mijini watu na wazidi kuwa wengi kama majani uwandani! Jina lake na liwepo kale na kale! Siku zote, jua likingali liko, jina lake na lichipuke, watu wa mataifa yote wajibariki na kulitaja pamoja na kulishangilia. Na atukuzwe Bwana Mungu, Mungu wa Isiraeli! Yeye peke yake ndiye afanyaye vioja! Jina lake tukufu na litukuzwe kale na kale! Nchi zote na zijae utukufu wake! Amin. Amin. Huu ndio mwisho wa maombo ya Dawidi, mwana wa Isai. Kweli Mungu huwaendea Waisiraeli kwa kuwa mwema, ni wao wenye mioyo iliyong'aa Lakini mimi ilikuwa imesalia kidogo, miguu yangu ingalijikwaa; hakuna tena iliyosalia, nyayo zangu zingaliteleza. Kwani wenye majivuno naliwaonea wivu nilipowaona wasiomcha Mungu, wakikaa na kutengemana. Kwa maana hawaoni maumivu ya kuwaua, tena miili yao hunenepa. Katika masumbuko ya kimtu hao hawamo, wala mateso ya watu wengine hayawapati. Urembo wao ndio majivuno, mavazi yao ya kujifunika ndio ukorofi. Macho yao hujitokeza kwa kunona kwao nyuso, mawazo ya mioyo yao hufuliza kujikuza. Kwa ukorofi wao mbaya husema na kufyoza, kila wanaposema hujikweza. Maneno ya vinywa vyao huyawazia kuwa ya kimbinguni, lakini ndimi zao husema ya kiulimwenguni. Kwa sababu hii watu wa kwao hurudi upande wao wakipenda kujinywesha maji yao mengi. Husema mioyoni: Mungu anavitambuaje? Uko utambuzi kwake yeye Alioko huko juu? Tazama, hivyo ndivyo, wasiomcha Mungu walivyo, ndivyo, wanavyojituliza kale na kale kwa kulimbika mali. Ni bure kweli, nikiuangalia moyo wangu, uwe umetakata, nikiinawa mikono yangu kwa maji yaondoayo makosa? Nikawa nimeteseka mchana kutwa, nayo mapatilizo yangu yalikuwa yako kila kulipokucha. Kama ningaliwaza kwamba; nami niseme kama wao hao, kweli walio kizazi cha watoto wako ningaliwaacha, nikavunja agano. Basi, nikayatia moyoni, niyatambua hayo; lakini nilipoyatazama, yakaniwia mazito, mpaka nikapaingia Patakatifu pake Mungu; ndipo, nilipoyatambua kwa kutazama, jinsi mwisho wao ulivyo. Kweli uliwaweka penye utelezi, ukawaangusha, wapondeke. Kumbe mara wameangamia na kutoweka kabisa! Mwisho wao ukawa wa kuustukia. Kama ndoto inavyoisha kwa kuamka, ndivyo, unavyozitowesha sura zao ukiwainukia. Hapo, nilipoona uchungu moyoni mwangu, nayo mafigo yangu yaliponiumiza na kunichoma, ndipo, mimi nilipokuwa jinga, nisijue kitu, nikawa machoni pako kama nyama. *Lakini sasa nitaandamana na wewe pasipo kukoma, maana umenishika kuumeni kwangu, ukaniongoza njia kwa shauri, ulilolipiga wewe, mwisho utanikaribisha huko, utukufu uliko. Huko mbinguni yuko mwingine aliye mwenzangu? Sipendezwi tena na ulimwengu huu nikiwa pamoja nawe. Ijapo, mwili wangu uzimie pamoja na moyo wangu, wewe Mungu u mwamba wa moyo wangu, tena u fungu langu la kale na kale. Hii ni kweli: Wakukaliao mbali hupotea, unawaangamiza wote wanaokuacha kwa kuzifuata tamaa. Lakini mimi naona kuwa vema, nikimkalia Mungu karibu. Bwana Mungu ninamtaka kuwa kimbilio langu, niwasimulie watu matendo yako yote.* Kwa sababu gani, Mungu, umetutupa kale na kale, moshi wa moto wa makali yako ukipanda kwao walio kondoo wako wa kuwachunga? Likumbuke kundi lako, ulilojipatia kale ulipolikomboa, liwe ukoo wako na fungu lako! Ukumbuke mlima wa Sioni, kao lako liliko! Inuka, uielekeze miguu yako kuja huku kulikobomolewa kale, maana adui wamefanya, patakatifu pawe pabaya pote. Wabishi wako hupiga makelele pako pa kukusanyikia, wakazitweka bendera zao, zionyeshe nguvu zao. Tukiwatazama, wamefanana na watu wainuao mashoka juu, wakate miti iliyoko mwituni. Sasa mapambo yake yaliyochorwa, yote pia wanayakatakata kwa mashoka na kwa nyundo. Numba yako takatifu wameichoma moto, wakalichafua Kao la Jina lako mpaka chini. Walisema mioyoni mwao kwamba: Na tuwamalize wote pamoja! Nyumba za Mungu zilizoko katika nchi hii wakaziteketeza zote. Vielekezo vyetu hatuvioni tena, wala hakuna mfumbuaji, Kweli hakuna kwetu ajuaye, kama vitakoma lini. Mungu, hao watusongao watutukane mpaka lini? Adui walisimange Jina lako kale na kale? Mbona mkono wako unaurudisha nyuma? Utoe mkono wako wa kuume kifuani pako, uje, uwamalize! Lakini Mungi ni mfalme wangu tangu zamani za kale, ndiye anayetengeneza wokovu huku nchini. Wewe uliitenga bahari kwa nguvu yako, ukavivunja vichwa vyao nyangumi waliomo majini. Wewe huviponda vichwa vyao wale papa wakubwa, ukawapa watu wakaao barani, wawalie chakula. Wewe hutoa mchangani visima, hata vijito, nayo majito yaliyokuwa yenye maji siku zote huyapwelesha wewe. Wako ni mchana, usiku nao ni wako; wewe ndiwe uliyeweka mbalamwezi nalo jua. Mipaka yote ya nchi wewe uliikata, ukaziumba siku za kiangazi nazo za kipupwe. Bwana, wakumbuke adui, ya kuwa hukutweza, nao watu wajinga hulibeza Jina lako. Roho ya hua wako usiitoe, nyama wa porini akaipata, wala usiwasahau kale na kale wanyonge wako, wawepo wenye uzima! Lile Agano liko, na ulitazame! Kwani maficho yote ya nchi yamegeuka kuwa makao ya ukorofi. Akorofikaye usimwache, ajiendee kwa kuona soni! Wanyonge na wakiwa ndio watakaolitukuza Jina lako. Inuka, Mungu, ujigombee kondo, kwani ni yako! Kumbuka, jinsi unavyotwezwa na wajinga siku zote! Usiyasahau makelele yao wabishi wako! Mafujo yao wakuinukiao yanaongezeka siku kwa siku. Twakushukuru, Mungu, twakushukuru, kwa kuwa Jina lako liko karibu, vioja vyako ndivyo vinavyolitangaza. Unasema: Itakapofika siku, niliyoiweka, mimi nitatoa maamuzi yanyokayo. Ijapo, nchi zitetemeke pamoja nao wazikaliao, mimi ndimi ninayezishikiza nguzo zake. *Niliwaambia wenye majivuno: Msijivune! Msielekeze mabaragumu juu, ninyi msionicha! Mabaragumu yenu msiyaelekeze juu kabisa, wala msinyoshe shingo mtakaposema! Kwani maawioni siko, wala machweoni siko, wala nyikani siko, ukuu utokako. Kwani Mungu ndiye anayeamua; yeye ndiye anayenyenyekeza, tena ndiye anayekweza.* Kwani mkononi mwake Bwana kimo kikombe kilichojaa mvinyo zichemkazo kwa viungo vikali, wote pia wasiomcha Mungu katika nchi huwagawia, wanywe, mpaka wafyonze mashimbi nayo. Lakini mimi nitamtangaza kale na kale, Mungu wake Yakobo nitamwimbia sifa. Nayo mabaragumu yao wasiomcha Mungu nitayavunja yote, lakini mabaragumu yao wamchao yataelekezwa juu. Kwa mwimbishaji, wa kuimbia mazeze. Wimbo wa Asafu wa kushukuru. Mungu hujulikana kwao Wayuda, Jina lake ni kubwa kwao Waisiraeli. Kituo chake kiko huko Salemu, nalo Kao lake liko huko Sioni. Huko ndiko, alikovunjia mishale ya upindi, hata ngao na panga na mata yo yote ya kupigia vita. Kwa utukufu wako wewe unaogopesha, maana huipita ile milima ya wanyang'anyi kwa kuwa mkubwa. Wenye mioyo mikali walitekwa nao, wakalala usingizi kwa kuangushwa wale wenye nguvu wote pia, mikono yao ikawalegea. Kwa makaripio yako, Mungu wa Yakobo, waliomo garini waliangushwa, wakazimia roho pamoja na farasi. Wewe unaogopesha kweli; atakayesimama mbele yako wewe, moto wa makali yako ukitokea, atapatikana wapi? Ulipotangaza maamuzi toka mbinguni, nchi ikashikwa na woga, ikanyamaza kimya; ndipo, Mungu alipoinuka kuwaamulia watu, apate kuwaokoa wanyonge wote walioko nchini. Kwani makali ya watu nayo hukutukuza, mwisho utauzima nao moto wa makali yao utakapojifunga. Mkimwapia, mlipeni Bwana Mungu wenu! Wote wakaao na kumzunguka sharti wampelekee matunzo, kwani yeye hutisha, aogopwe sana, huzikata roho zao walio wakuu, nao wafalme wa nchi huwaogopesha. Kwa mwimbishaji. Wimbo wa Asafu, aliomtungia Yedutuni. Nimpaliziaye sauti yangu, ndiye Mungu; ninapomwita Mungu, hunisikiliza. Siku ya kusongeka kwangu nilimtafuta Bwana; mikono yangu ikawa imenyoshwa usiku kucha pasipo kulegea, maana roho yangu ilikataa kutulizwa. Nikimkumbuka Mungu nampigia kite, roho yangu ikitaka kuzimia, ninayawaza yote. Unayashika macho yangu, yasisinzie; lakini siwezi kusema kwa kuhangaika. Ndipo, ninapoyawaza yale mambo ya siku za kale, ndiyo yale ya ile miaka iliyokwisha kupita. Usiku nayakumbuka mazeze yangu humu moyoni mwangu, roho yangu ikitafuta njia ya kuyatambua hayo: Bwana atanitupa kale na kale? Hataendelea tena kunipendezesha? Huruma yake imekwisha kale na kale? Agano, aliloliwekea vizazi na vizazi, limekoma? Mungu ameyasahau magawio ya kuwapa watu? Au ameukataza upole wake kwa kukasirikia? Nikasema: Maumivu haya yananipasa, ni miaka ya mkono wake wa kuume yule Alioko huko juu. Haya matendo ya Bwana nitayakumbuka, navyo vioja vyako vya kale nitavikumbuka kweli. Ninayaweka moyoni yote, uliyoyafanya, nipate kuziwaza vema hizo kazi zako. Njia yako, Mungu, ni takatifu; yuko wapi aliye mungu mkuu kama Mungu? Wewe ndiwe Mungu afanyaye vioja, nguvu zako hutambulikana kwa koo za watu. Uliwakomboa kwa mkono wako walio ukoo wako, hawa wana wa Yakobo nao wa Yosefu. Yalipokuona, Mungu, maji ya bahari, yalipokuona majihayo, ndipo, yalipostuka, vilindi navyo vikatetemeka. Mawingu yakanyesha mvua yenye maji mengi, mishale yako ikapiga huko na huko, nako mbinguni kukanguruma, Sauti za ngurumo zako zikasikilika katika kimbunga, nchini pakamulikwa na umeme, nchi ikatetemeka na kuyumbayumba. Namo baharini ndimo, njia yako ilimo, nako kwenye maji mengi ukapita, lakini nyayo zako hazikutambulika. Walio ukoo wako uliwaongoza kama kundi la kondoo kwa mikono yao hawa: Mose naye Haroni. Ninyi mlio ukoo wangu, yasikilizeni mafundisho yangu! Yategeni masikio yenu, msikie, kinywa changu kinavyoyasema! Nitakifumbua kinywa changu, kiseme mifano na kuwaambia mafumbo yaliyo ya kale. Tuliyasikia, tukayajua, maana waliotusimuliani baba zetu. Nasi tusiyafiche wana wao, wao wa vizazi vijavyo tuwasimulie mashangilio ya Bwana nayo matendo yake ya nguvu ya kustaajabisha, aliyoyafanya yeye. Alisimika mashuhuda kwao Wayakobo, akaweka maonyo kwao Waisiraeli, akawaagiza baba zetu, wayafundishe, wana wao wayajue, kusudi wao wa vizazi vijavyo nyuma wayajue nao, kwamba nao watakapokua wayasimulie watoto wao, wapate kumwegemea Mungu na kumjetea, wasizisahau kazi zake Mungu, wayashike maagizo yake, wasiwe kizazi, kama hicho cha baba zao: chenye ubishi na ukatavu, chenye mioyo isiyopaelekea hapo pamoja, tena chenye roho zisizomtegemea Mungu. Wana wa Efuraimu walikuwa mafundi wa kupiga mishale, lakini siku ya kupiga vita walirudi nyuma. Agano la Mungu hawakulishika, wakakataa kuyafuata Maonyo yake. Wakayasahau matendo yake, hata vioja vyake, alivyowaonyesha. Alifanya vioja machoni pao baba zao katika nchi ya Misri shambani kwa Soani. Alipasua bahari, akawapitisha mlemle akiyasimamisha maji yake kuwa kama ukingo. Akawaongoza mchana kwa wingu, nao usiku wote kwa mwanga wa moto. Akapasua magenge kule nyikani, akawapa maji mengi ya kunywa, kama viko vilindi. Kulikokuwa na miamba tu ndiko, alikotokeza vijito, akavifurikisha maji, yatelemke kama ya mito mikubwa. Kisha wakafuliza kumkosea tena, wakakataa jangwani kumtii yule Alioko huko juu. Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao, wakitaka kwake vilaji viwapendezavyo rohoni mwao. Wakamnung'unikia Mungu wakisema: je? Mungu ataweza kututandikia meza huku nyikani? Kweli alipopiga mwamba, maji yakatoka, vijito vikaenda; lakini atawezaje kutupa navyo vilaji? nazo nyama atatupatiaje sisi tulio ukoo wake? Naye Bwana alipovisikia alichafuka sana, moto ukawashwa wa kuwala wao Wayakobo, makali yakawafokea wao Waisiraeli. Kwani hawakumtegemea yeye Mungu, wala hawakungojea, awaokoe. Naye akaagiza mawingu yaliyoko juu, akaifungua milango ya mbinguni, akawanyeshea Mana, wapate kula; ndio ngano zambinguni, alizowapa. Wakala kila mtu huo mkate wa malaika; hivyo aliwapelekea pamba za njiani za kushiba. Kisha akatokeza mbinguni upepo wa maawioni kw ajua, akauvuta nao upepo wa kusini kwa nguvu zake. Akawanyeshea mvua kama ya mavumbi, ndio nyama wa kula, ni ndege warukao, wengi mno kama mchanga wa ufukoni. Akawaangusha kambini kwao po pote, walipokuwa wamepanga. Wakala, wakashiba sana, alipowapa, wazikomeshe tamaa zao; lakini hizo tamaa zao hawakuziacha, hivyo vilaji vyao vilipokuwa vikingalimo vinywani mwao bado. Hapo ndipo, makali ya Mungu yalipomkwea kwa ajili yao, waliokuwa wenye nguvu akawaua, nao vijana wa Isiraeli akawalaza uvumbini. Katika mambo hayo yote wakamkosea tena, hata vioja vyake hawakuvitegemea. Kwa hiyo alizimaliza siku zao upesi, wakawa kama mvuke, miaka yao ikapita upesi sana, alipowaangamiza kwa mastuko. Napo hapo, alipowaua hivyo, ndipo, walipomtafuta, wakarudi na kumtazamia machana kutwa. Wakamkumbuka Mungu kuwa mwamba wao, ya kuwa yeye Alioko huko juu ni mwokozi wao. Lakini hata hapo walimdanganya na vinywa vyao, nazo ndimi zao zikamwongopea; nayo mioyo yao haikumwelekea, wala Agano lake hawakulitegemea. Lakini kwa kuwahurumia akazifunika manza zao, asiwaangamize, akayarudisha makali yake, yaende nyuma kabisa, asiuchochee moto wote wa machafuko yake. Akawakumbuka kuwa wenye miili ya kimtu tu, kuwa upepo upitao pasipo kurudi. Je? Mara ngapi walimchokoza nyikani, wakamsikitisha jangwani? Mara kwa mara walirudi nyuma, wamjaribu Mungu; ndivyo, walivyomsumbua Mtakatifu wa Isiraeli. Hawakukumbuka, ya kuwa ni mkono wake uliowakomboa siku ile ulipowatoa mikononi mwake aliyewasonga. Naye ndiye aliyevifanya vielekezo vyake katika nchi ya Misri, navyo vioja vyake shambani kwa Soani: maji ya mito yao aliyageuza kuwa damu, wasiweze kuyanywa yale maji yao. Akatuma kwao mbu, wawale, hata vyura, wawamalize. Mashamba yao akawapa funutu, navyo, vyakula, walivyovipanda na kusumbuka, akawapa nzige. Mizabibu yao akaivunja kwa mvua ya mawe, kwa hiyo mvua ya mawe ikafa nayo mikuyu yao. Hata ng'ombe wao akawatoa, wapigwe nayo hiyo mvua ya mawe, nao mbuzi wao akawamaliza kwa umeme. Akatuma kwao moto wa makali yake, tena machafuko na machungu na masongano mengine; lilikuwa kundi zima la malaika waliowapelekea mabaya. Akayafungua makali yake, yajiendee tu, hakuzitoa roho zao katika kufa, ila aliwaacha, kipindupindu kiwashike, wajifie. Akampiga kila mzaliwa wa kwanza katika nchi ya Misri, wote waliokuwa malimbuko yenye nguvu katika mahema ya Hamu. Lakini walio ukoo wake walitoka, akiwachunga kama kondoo, akawaongoza kama kundi la mbuzi huko nyikani, akawasafirisha vizuri, wasishikwe na woga, lakini adui zao bahari iliwafunika. Akawafikisha kwenye mpaka wa Patakatifu pake, penye ule mlima, ambao ulijipatia mkono wake wa kuume. Akawafukuza wamizimu mbele yao, akawaagiza kugawiana nchi zao kwa kuzipigia kura, kila apate fungu lake, ndilo liwe urithi wake, akayakalisha mashina ya Isiraeli katika mahema yao. Lakini walimjaribu Mungu alioko huko juu na kumchokoza, hawakuyashika maagano yake, aliyoyashuhudia, wakarudi nyuma kwa udanganyifu wao kama baba zao, wakapinduka kama upindi usiotegemeka. Kwa kutambika vilimani juu wakamkasirisha, kwa kuvitambikia vinyago vya wakamtia wivu. Moto wa makali ukamkwea Mungu, alipoyasikia, akawatupa Waisiraeli kabisa kabisa. Akaliacha Kao lake kule Silo, ni lile hema, ambalo alikaa humo kwenye watu. Wale, aliowatia nguvu, akawatoa, wafungwe, waliokuwa urembo wake akawatia mikononi mwao waliowasonga. Walio ukoo wake akawaacha, wauawe na panga, wao waliokuwa fungu lake akawatolea makali yake. Moto ukawala vijana wao wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za ndoa. Watambikaji wao wakauawa kwa panga, nao wajane wao hawakuwaombolezea. Kisha Bwana aliamka kama mtu aliyelala usingizi, kama mwenye nguvu anayepiga shangwe akiondoka kwenye mvinyo. Akawapiga waliowasonga, akawarudisha nyuma, nayo masimango ya kale na kale ndiyo, aliyowapatia. Akakitupa kituo cha Yosefu, nao ukoo wa Efuraimu hakuuchagua. Akauchagua ukoo wa Yuda na mlima wa Sioni, alioupenda. Akapajenga Patakatifu pake, paende juu kabisa, pawe kama nchi, aliyoiweka ya kuwapo kale na kale. Kisha akamchagua mtumishi wake Dawidi, aje kumtumikia; kwenye mazizi ya kondoo ndiko, alikomchukua. akamtoa kwenye kondoo wanyonyeshao, awachunge walio ukoo wake Yakobo pamoja nao walio fungu lake Isiraeli. Akawachunga kwa kuwa mwenye moyo uliotakata wote, kwa kuwa mikono yake iliijua kazi hiyo, akawaongoza. Mungu, wamizimu wameuingia mji ulio fungu lako, wakalichafua Jumba lako lililo takatifu, Yerusalemu wakaugeuza kuwa mabomoke tu. Mizoga ya watumishi wako wameitoa, iliwe na ndege wa angani, nayo miili yao wlaiokucha wamewapa nyama wa porini. Damu zao wakazimwaga kama maji, zizunguke Yerusalemu, tena hakuna aliyewazika hao waliokufa. Majirani zetu tunaona soni kwao, maana watuzungukao wanatufyoza na kutusimanga. Bwana, mpaka lini utatukasirikia? Itakuwa kale na kale? Wivu wako unachoma kama moto uwakao. Makali yako wamwagie wamizimu wasiokujua, nazo nchi zenye wafalme wasiolitambikia Jina lako! Kwani wamemla Yakobo, wakapabomoa, walipokuwa amekaa. Usizikumbuke manza, baba zetu walizozikora, ukitulipisha sisi! Huruma zako na zije kutufikia upesi! Kwani tumelegea sana. Mungu uliye mwokozi wetu, tusaidie, kwa ajili ya utukufu wa Jina lako tuopoe, kwa ajili ya Jina lako yafunike makosa yetu! mbona wamizimu waseme: Mungu wao yuko wapi? Sharti tuvione na macho yetu, vikitambulikana kwao wamizimu, jinsi unavyozilipiza damu zilizomwagwa za watumishi wako. Sharti hivyo, walio kifungoni wanavyopiga kite, vifike mbele yako, kwa nguvu zamkono wako zilizo kuu uwaokoe kufani hao wanao! Majirani zetu uwarudishie mara saba vifuani mwao vyote, walivyokusimangia wewe, Bwana! Ndipo, sisi tulio ukoo wako na kindoo, unaowachunga, tukapokutolea shukrani kale na kale, tukisimulia vizazi na vizazi, ya kuwa inapasa kukushangilia. Kwa mwimbishaji, auimbishe kama wimbo wa kwamba: Maua ya porini hushuhudia. Wimbo wa Asafu Mchungaji wa Isiraeli, sikiliza! Wewe umchungaye Yosefu, kama ni kundi la kondoo, wewe ukaaye juu ya Makerubi, utokeze mwanga wako, Efuraimu na Benyamini na Manase na waone, jinsi unavyoziamsha nguvu zako kuu ukija kutuokoa! Wewe Mungu, turudishe kwako! Utuangazie uso wako! Ndivyo, tutakavyookoka. Bwana Mungu Mwenye vikosi, utakasirika mpaka lini, ijapo wakulalamikie walio ukoo wako? Umewalisha mikate iwalizayo, nayo machozi yao yakawa vinywaji, ulivyowanywesha kwa vikombe. Umetuacha, majirani zetu wakapigana wao kwa wao, watupate sisi, nao adui zetu wanatusimanga. Mungu Mwenye vikosi, turudishe kwako! Utuangazie uso wako! Ndivyo, tutakavyookoka. Uko mzabibu, ulioung'oa kule Misri; ukafukuza wamizimu, ukaupanda mahali pao. Ukaupanulia, uweze kutia mizizi yake, ukaieneza nchi. Milima ikafunikwa na kivuli chake, nayo miangati ya Mungu ikafunikwa na matawi yake mengi. Ukayaendesha machipukizi yake mpaka baharini, nayo miche yake ukaifikisha kwenye mto mkubwa. Mbona umekibomoa kitalu chake, wote wapitao njia wakapata kuuchuma? Nguruwe wa mwituni wakauchimbachimba, nao nyama wa porini wakaula. Mungu Mwenye vikosi, tunakuomba: Rudi! Chungulia toka mbinguni, uvione! Huo mzabibu wako uutazama! Uuangalie! Maana mkono wako wa kuume ndio ulioupanda, ni mwanao, uliyemkuza na kumpa nguvu. Umechomwa na moto, ukakatwakatwa; lakini kwa makaripio ya uso wako wataangamia. Mtu, mkono wako wa kuume uliyemweka, mkono wako na umshike! Na umshike huyo mwana wa mtu, uliyemkuza na kumpa nguvu! Nasi hatutaki kuondoka kwako wewe; kusudi tupate kulikuza Jina lako, tupe uzima tena! Bwana Mungu Mwenye vikosi, turudishe kwako! Utuangazie uso wako! Ndivyo, tutakavyookoka. Kwa mwimbishaji, wa kuimba kama wimbo wa wagemaji. Wa Asafu. Mpigieni Mungu shangwe, maana ni nguvu yetu! Mungu wa Yakobo mpigieni vigelegele! mwimbieni nyimbo za kumshukuru na kupiga patu! Pigeni nayo mazeze yaliayo vizuri pamoja na mapango! Pigeni mabaragumu, mwezi ukiandama! Hata penye mbalamwezi! Ndio sikukuu yetu. Kwani Isiraeli alivyoagizwa, ndivyo hivyo, navyo ndivyo vimpasavyo Mungu wa Yakobo; ndio ushuhuda, aliouweka kwao wa Yosefu, alipotokea katika nchi ya Misri, aipige. Hapo ndipo, niliposikia msemo, niliokuwa sijaujua: Huo mzigo wa begani kwake nimeuondoa, mikono yake ikaondoka kwenye makapu ya kuchukulia watu. Uliponililia katika masongano, nimekuponya, nikakuitikia na kujificha katika mawingu yenye ngurumo, kwenye Maji ya Magomvi nikakujaribu. Sikilizeni, mlio wa ukoo wangu, niwaonye! Isiraeli, sharti unisikie! Kwako kusiwe tena na mungu mgeni! Wala usitambikie mungu wa nchi nyingine! Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri ni mimi Bwana; kiasame kinywa chako, nikijaze! Lakini walio ukoo wangu hawakuisikia hiyo sauti yangu, naye Isiraeli hakutaka kunifuata mimi. Nikawaacha, waufuate ugumu wao wa mioyo yao, wajiendee na kuyafanya mashauri yao. Kama wangekuwa ukoo wangu, wangenisikia, kama wangekuwa Waisiraeli, wangezishika njia zangu, nami ningewainamisha upesi adui zao, mkono wangu ungewarudia wao waliowasonga. Wachukivu wake Bwana wangemnyenyekea, lakini wao siku zao zingekuwa za kale na kale. Ningewapa ngano zilizo nzuri kupita zote, wazile zizo, ningewapa hata asali za miambani, wazile, mpaka washibe. Mungu anasimama katika mkutano wao miungu mwingine, atoe hukumu katikati yao hiyo miungu. Mpaka lini mtayapotoa maamuzi yenu mkiwa upande wao wasionicha? Waamulieni wakorofikao nao wafiwao na wazazi! Wanyonge na maskini watengenezeeni mashauri kwa wongofu! Waopoeni wakorofikao nao wakiwa mkiwatoa mikononi mwao wasionicha! Lakini hawavitambui, wala hawaonyeki, ila hujiendea gizani, ijapo, shikizi zote za nchi zije kutikisika. Mimi nilisema: Ninyi m miungu, nyote m wanawe Alioko huko juu. Lakini mtakufa kweli kama wana wa watu, mtaanguka kama m wenzao walio wakuu. Inuka, Mungu! Ihukumu nchi! Kwani mwenye wamizimu wote ndiwe wewe. Mungu usijinyamazie tu! Wala usiache kujibu! Usitulie tu, wewe Mungu! Kwani tazama, adui zako wanafanya fujo! Wachukivu wako wanainua vichwa! Wanakula njama ya kuwaangamiza walio ukoo wako, wanawapigia mashauri mabaya wao, uliowaficha. Wanasema: Njoni, tuwang'oe, kabila lao life! Jina la Isiraeli lisikumbukwe tena! Kweli mioyo yao wote ililipatana neno hili moja, wakafanya maagano, wakupelekee vita. Ni wao wakaao katika mahema: Waedomu na Waisimaeli, Wamoabu nao wao walio Wahagri, tena Wagebali na Waamoni, nao Waamaleki, Wafilisti pamoja nao wakaao Tiro. Katika hilo shauri lao wakajitia nao Waasuri; nao ndio wanaowatumikia wana wa Loti kuwa mikono yao. Kama ulivyowafanyizia Wamidiani, wafanyizie nao, au kama ulivyomfanyizia Sisera na Yabini kule mtoni kwa Kisoni! Kule Endori ndiko, walikoangamizwa, wakawa mbolea tu ya kuotesha mchanga. Hivyo, ulivyomfanyizia Orebu na Zebu vifanyizie wakuu wao! Vile vya Zeba na Salmuna, vifanyizie wafalme wao wote! Ndio waliosema: Na tuyateke makao yake Mungu, yawe yetu sisi! Mungu wangu, wafanye kuwa mavumbi yachukuliwayo na kimbunga au kuwa makapi, yakipeperushwa na upepo, wawe kama moto unaochoma mwitu, au kama ndimi za moto ziwashazo milima! Vivyo hivyo uwakimbize kwa nguvu zako zilizo za kimbunga! Uwastushe, wazimie kwa nguvu zako zilizo za chamchela! Nyuso zao sharti ziwaive kwa kutwezwa, mpaka walitafute Jina lako, wewe Bwana. Sharti wapatwe na soni pamoja na mastuko kale na kale! Sharti waumbuliwe, mpaka waangamie! Ndivyo, watu watakavyolitambua Jina lako kuwa Bwana, kwa kuwa wewe peke yako u mkuu katika nchi zote. Kwa mwimbishaji, wa kuimba kama wimbo wa wagemaji? Wimbo wa wana wa Kora. *Hapo, unapokaa, Bwana Mwenye vikosi, ndipo pazuri peke yake. Roho yangu ilitaka kuzimia kwa kuzitunukia nyua za Bwana; moyo wangu na mwili wangu unamshangilia Mungu Mwenye uzima. Kumbe ndege ameona nyumba, kinega akajipatia kiota, ndimo, atakamozaa makinda yake: ndipo, unapotambikiwa wewe, Bwana Mwenye vikosi, uliye mfalme wangu na Mungu wangu. Wenye shangwe ndio wakaao katika Nyumba yako, wanaokushangilia pasipo kukoma. Wenye shangwe ndio wajitafutiao nguvu kwako wewe, wawazao mioyoni mwao, jinsi watakavyofika kwako. Ijapo, wapite katika bonde lilizalo wengine, hulitumia kuwa kisima cha kuwanywesha maji, kwani mvua ya vuli hulichipuza nalo na kulipatia mbaraka. Huendelea na kuongeza nguvu mara kwa mara, mpaka wamtokee Mungu kule Sioni na kumwambia: Bwana Mungu Mwenye vikosi, sikiliza ninayokuomba! Tega masikio, Mungu wa Yakobo! Mungu uliye ngao yetu, unitazame, uuone uso wake uliyempaka mafuta! Kwani siku moja ya kukaa katika nyua za Bwana ni nzuri kuliko nyingine, ijapo ziwe elfu. Kungoja zamu mlangoni kwa nyumba ya Mungu kwanipendeza kuliko kukaa mahemani kwao wasiomcha Mungu. Kwani Bwana Mungu ni jua na ngao, Bwana hutugawia nao utukufu, wanaoendelea wakimcha hawanyimi chema cho chote. Mtu akuegemeaye, Bwana Mwenye vikosi, ndiye mwenye shangwe.* Bwana, ulikuwa umependezwa na nchi yako, tena ulikuwa umerudisha mateka yake Yakobo. Walio ukoo wako ukawaondolea manza, walizozikora, makosa yao yote ukayafunika. Machafuko yako yote ukayatuliza na kuuzima moto wa makali yako. Mungu uliye mwokozi wetu, uturudishe! Ukomeshe uchungu, ulio nao kwa ajili yetu! Makali yako yatukalie kale na kale? Au utayaeneza hayo makali yako, yafikie vizazi na vizazi? Hutatuchangamsha tena, kwa kuturudisha uzimani, walio ukoo wako wakufurahie? Bwana, tupe kuuona tena huo upole wako, ukitugawia wokovu wako sisi nasi! Mungu Bwana atakayoyasema, ninataka kuyasikia, kwani wao walio ukoo wake nao wanaomcha huwaambia maneno yenye utengemano, wasirudie tena ujinga wao. Kweli wokovu wake uko karibu kwao wamwogopao, utukufu upate kukaa katika nchi yetu. Upole na welekevu sharti ukutaniane, nao wongofu na utengemano sharti unoneane! Ndivyo, welekevu utakavyochipuka katika nchi, wongofu ukiitazama toka juu mbinguni. Ndipo, Bwana atakapotupa hayo mema tena, ndipo, nchi yetu nayo itakapotupa mazao yake tena. Utakaokwenda mbele yake ndio wongofu, tena ndio utakaofuata hapo, alipopita, upatengeneze kuwa njia.* Bwana, liinamishe sikio lako, uniitikie! Kwani mimi ni mnyonge, hata mkiwa. Ilinde roho yangu! Kwani mimi ninakucha. Wewe Mungu wangu, mwokoe mtumishi wako aliyekuegemea! Wewe Bwana, nihurumie! Kwani ninakulilia mchana kutwa. Roho ya mtumishi wako ifurahishe! Kwani ninakuinulia roho yangu, ikutazamie, Bwana. Kwani wewe Bwana u mwema, unapenda kuondoa makosa, upole wako ni mwingi kwao wakuliliao. Sikia, Bwana, ninayokuomba! Sauti ya malalamiko yangu itegee masikio! Siku, ninaposongeka, ninakuita, kwani unaniitikia. Miongoni mwa miungu hayumo aliye kama wewe, Bwana, hayumo awezaye kufanya matendo kama yako. Wamizimu wote, uliowafanya, watakuja, wakuangukie, nalo Jina lako, Bwana, watalitukuza. Kwani wewe u mkubwa, unafanya mataajabu, aliye Mungu niwewe peke yako. Nifundishe, Bwana, njia yako, niendelee na kweli yako! Ushike moyo wangu, upende moja tu: kuliogopa Jina lako! Nitakushukuru, Bwana Mungu wangu, kwa moyo wote na kulitukuza Jina lako kale na kale. Kwani upole wako, ulionitolea umekuwa mkubwa, ukaiopoa roho yangu kuzimuni chini ya nchi. Mungu, wako wenye majivuno walioniinukia, ni kundi zima la wakorofi, wanaitafuta roho yangu, lakini wewe hawakutaki kuwa machoni pao. Nawe wewe Bwana u Mungu mwenye huruma na utu, tena u mwenye uvumilivu na upole na welekevu mwingi. Rudi upande wangu na kunihurumia! Mpe mtumishi wako nguvu ya kwako! Mwana wa mjakazi wako umwokoe! Nifanyizie kielekezo kinipatiacho mema, wachukivu wangu wakione, waingiwe na soni, kwa kuwa wewe Bwana umenisaidia, ukanituliza moyo. Ulijengwa na kushikizwa kwenye milima iliyo mitakatifu. Bwana huipenda milango wa Sioni kuliko makao yote ya Yakobo. Mambo yenye utukufu hutangazwa mwako ulio mji wa Mungu. Nitakumbusha Rahabu na Badeli miongoni mwao wanijuao, waliozaliwa mumo humo watazameni: wamo Wafilisti na Watiro, hata Wanubi! Sioni hutukuzwa kwamba: Watu wa makabila yote huzaliwa mle! Naye Alioko huko juu ndiye anayeushupaza. Bwana akiyahesabu makabila ya watu ataandika kwamba: Fulani na fulani walizaliwa mlemle. Nao wenyewe watacheza ngoma pamoja na kuimba: Visima vyangu vyote vimo mwako! Wimbo wa wana wa Kora, waliomtungia mwimbishaji, auimbishe kama wimbo wa kwamba: Ugonjwa huinamisha. Fundisho la Hemani aliye wa ukoo wa Ezera. Bwana Mungu uniokoaye, mchana ninakulilia, usiku nao sikuachi, sharti yafike kwako malalamiko yangu. Liinamishe sikio lako, nikikupigia kelele! Kwani roho yangu imeshiba kwa kuona mabaya, uzima wangu umekwisha, kuzimu kumenijia karibu. Ninahesabiwa kuwa mwenzao washukao shimoni, nimegeuka kuwa kama mtu asiye na nguvu hata kidogo. Kilalo changu kiko kwao waliokwisha kufa, ninafanana nao waliouawa vitani walalao makaburini; huwakumbuki tena waliokwisha kutengwa, watoke mkononi mwako. Umenilaza shimoni ndani ya nchi kwenye giza lililomo humo kuzimuni. Makali yako yamenilemea, mawimbi yako yote yamenikwelea. Wenyeji wangu umewahamisha, nisiwaone, ukaniweka kuwa tapisho kwao hao; hivyo, nilivyofungwa, sitaweza kutoka. Macho yangu yamefifizwa kwa kuumia, ninakulilia, Bwana, mchana kutwa na kukunyoshea wewe mikono yangu. Je? Utafanya kioja kwenye wafu? Au vivuli vitainuka, vikushukuru? Je? Mambo ya upole wako yanasimuliwa makaburini? Au mambo ya welekevu wako yanasimuliwa kuzimuni? Je? Vioja vyako vinatambulikana kwenye giza? Au wongofu wako katika nchi ikaayo walioyasahau yote? Lakini mimi ninakupigia kelele wewe, Bwana, malalamiko yangu hufika kwako asubuhi na mapema. Mbona unaitupa roho yangu, wewe Bwana? Mbona unauficha uso wako, nisiuone? Mimi ni mnyonge na mwele toka utoto wangu, nikayavumilia mastuko yako, kisha nikazimia. Makali yako yenye moto yamenikwelea, matetemeko yako yakanizimisha roho. Yalinizunguka siku zote kama maji, yakanizinga na kunisonga pawapo pote. Wenzangu wapendwa umewahamisha, nisiwaone tena; wenyeji wangu waliosalia ni giza tupu. Magawio ya Bwana nitayaimbia kale na kale, vizazi na vizazi nitawajulisha kwa kinywa changu welekevu wako. Kwani nasema: Upole wako utajengewa kale na kale, mbinguni uliusimika welekevu wako, uwapatie watu nguvu. Ukasema: Niliagana naye niliyemchagua, mtumishi wangu Dawidi nikamwapia kwamba: Walio uzao wako nitawatia nguvu kale nakale, nikijenge kiti chako cha ufalme, kiwe cha vizazi na vizazi. Ndipo, mbingu zilipoyatukuza mataajabu yako, Bwana, welekevu wako ukatukuzwa nao kwenye mkutano wa watakatifu. Kwani kule mawinguni yuko nani aliye mkuu kama Bwana? Nako kwenye wana wa Kimungu yuko nani afananaye na Bwana? Watakatifu wakusanyikapo, Mungu huogopesha, nao wote wamzungukao hushikwa na woga. Bwana Mungu Mwenye vikosi, yuko nani aliye hivyo, ulivyo? U Bwana mwenye nguvu, welekevu wako unakuzunguka. Unayashinda hata majivuna yake bahari, mawimbi yake yakiumuka, unayatuliza. Wewe ulimponda Rahabu, akaanguka kama mtu aumizwaye vitani, kwa mkono wako wenye nguvu ukawatapanya adui zako. Mbingu ni zako, nchi nayo ni yako, kwani nchi navyo vyote vilivyoko ulivishikiza wewe. Vilivyoko kaskazini navyo vilivyoko kusini wewe uliviumba, milima ya Tabori na ya Hermoni inalipigia Jina lako shangwe. Mkono wako ni wenye uwezo sanasana, maganja yako nayo ni yenye nguvu, mkono wako wa kuume hutukuka. Wongofu unyoshao maamuzi ni msingi wa kiti chako cha kifalme, upole na welekevu huutangulia uso wako. Watu wajuao kushangilia ndio wenye shangwe, huendelea katika mwanga wa uso wako, Bwana. Jina lako wanalipigia vigelegele siku zote, maana kwa wongofu wako walipata ukuu. Kwani utukufu wa nguvu zao ni wewe, Bwana. mapenzi yako ndiyo yatupayo kuyaelekeza mabaragumu yetu juu. Kwani aliye mwenye ngao yetu ndiye Bwana, naye mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Isiraeli. Kale ulisema katika njozi nao waliokucha, ukawaambia: Yuko mwenye nguvu, niliyempa ushindaji; niliyemchagua nimemkweza, awapite wote ukuu. Nimemwona Dawidi, awe mtumishi wangu, nikampaka mafuta yangu yaliyo matakatifu. Maganja yangu yatamshikiza, kweli mkono wangu utamtia nguvu. Hakuna adui atakayemshinda na kumwogopea, wala hakuna mkorofi atakayemtesa. Mimi nitawapiga wamsongao, wakimbie watakapomwona, nao wachukivu wake nitawakumba, waanguke. Welekevu wangu na upole wangu utamkalia, kwa nguvu ya Jina langu atalielekeza baragumu lake juu. Mikono yake nitaifikisha kwenye bahari, mkono wake wa kuume sharti uje kwenye mito mikubwa. Yeye ataniita na kuniambia: Baba yangu ni wewe, u Mungu wangu nao mwamba ulio wokovu wangu. Mimi nami nitampa uzaliwa wa kwanza, na ukuu wa wafalme wa nchini. Kale na kale nitamwendea kwa upole wangu, nalo agano tuliloliagana, halitatanguka. Mazao ya kuwa ya kale na kale ndiyo, nitakayompa, nazo siku za kiti chake cha kifalme zitakuwa kama za mbingu. Watoto wake wakiyaacha Maonyo yangu, wasiendelee na kuyafanya yanyokayo machoni pangu, wakiyapinga maongozi yangu, wasiyaangalie maagizo yangu, Nitawaonya na kuwapiga fimbo kwa kukataa kunitii, hayo maumivu yawlaipishe manza zao, walizozikora. Lakini upole wangu sitawanyima, wala sitageuka kuwa mwongo, welekevu wangu ukiwaacha. Wala Agano langu sitalitangua, wala sitayageuzageuza yaliyotoka midomoni mwangu. Neno moja nimejiapia kwa utakatifu wangu, nami sitamwongopea Dawidi, ni lile la kwamba: Uzao wake utakuwa wa kale na kale, nacho kiti chake cha kifalme kitakuwa kama jua machoni pangu, kitakaa na nguvu yake kale na kale kama mwezi. Naye shahidi alioko huko juu mawinguni ni mwelekevu. Kisha wewe umemtupa na kumkataa; yeye, uliyempaka mafuta, umemchafukia. Agano, uliloliagana na mtumishi wako, umeliacha, urembo wake wa kichwani umeuchafua na kuutupa chini. Umevivunja vitalu vyake vyote pia, maboma yake yote umeyatoa, yabomolewe. Wote wapitao njia wanajipatia mateka papo hapo, naye amegeuka kuwa mtu wakusimangwa tu kwao, aliokaa nao. Umeikweza mikono yao ya kuume wao wamsongao, adui zake wote umewafurahisha. Hata ukali wa upanga wake umeurudisha nyuma, usipompa kusimama kwenye mapigano. Umeukomesha uzuri wake wa kifalme, usiwepo tena, nacho kiti chake cha kifalme umekibwaga chini. Siku za ujana wake umezifupiza, ukamtia soni, zimfunike kama nguo. Bwana, utajificha hivyo mpaka lini? Moto wa makali yako uwake kale na kale? Zikumbuke siku zangu, jinsi zinavyoishia upesi! Mbona wana wa watu wote ulijiumbia, wawe wa bure? Ni mtu gani anayekuwapo pasipo kuona kufa? Ni mtu gani atakayeiopoa roho yake katika nguvu za kuzimuni? Bwana, magawio ya upole wako ya kwanza yako wapi sasa? Tena ulimwapia Dawidi kwa welekevu wako, ayapate! Wakumbuke, Bwana, watumishi wako, jinsi wanavyosimangwa! Nayavumilia moyoni mwangu mabezo yamakabila yote, nayo ni mengi. Bwana, ndivyo, wanavyokusimanga wachukivu wako, tena ndivyo, wanavyozisimanga nazo nyayo zake, uliyempaka mafuta! Bwana na atukuzwe kale na kale! Amin. Amin. Bwana, wewe ndiwe kimbilio letu kwa vizazi na vizazi. Milima ilipokuwa haijazaliwa bado, hata nchi na ulimwengu zilipokuwa hazijaumbwa bado, wewe Mungu ulikuwa uko tangu kale hata kale. Unawageuza watu kuwa mavumbi tena ukiwaambia: Rudini, ninyi wana wa watu! Kwani machoni pako miaka elfu ni kama siku ya jana, ikiisha kupita, au kama zamu moja ya usiku. Kama watu wanavyochukuliwa na maji, ndivyo, unavyowadidimiza; kama usingizi wa asubuhi ulivyo, ndivyo, walivyo nao, au kama maua yanayochanua upesi: asubuhi hupasua na kuchanua, jioni hupakatika na kunyauka. Kwani tunamalizika kwa makali yako, maana tunatoweshwa na moto wa machafuko yako. Manza, tulizozikora, unaziweka machoni pako, makosa, tuliyoyaficha, hutokea mwangani mwa uso wako. Kwa hiyo siku zetu zote zinapita upesi kwa machafuko yako, tunaimaliza miaka yetu kuwa kama mapuzi tu. Siku zetu za kuwapo ni miaka sabini, kama tunazidi kuwa wenye nguvu, ni miaka themanini. Nayo masumbuko na mateso ndio urembo wao; kwa kuwa tunaruka kama ndege, zinapita upesi. Lakini yuko nani azitambuaye nguvu za makali yako? Tena yuko nani ayaogopaye hayo machafuko yako? Tufundishe kuzihesabu siku zetu, tujipatie mioyo yenye ujuzi! Rudi, Bwana! Utatukalia mbali mpaka lini? Walio watumishi wako wahurumie! Tushibishe upole wako kila kunapokucha! Ndivyo, tutakavyoshangilia kwa furaha siku zetu zote. Siku za kutufurahisha ziwe sawasawa nazo, ulizotutesa, ziwe miaka mingi, kama ilivyokuwa ile ya kuona mabaya. Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, nao utukufu wako kwa wana wao! Nao wema wake Bwana Mungu wetu na utukalie! Kazi za mikono yetu zifanikishe kwetu! Kazi za mikono yetu uzifanikishe kweli!* Akaaye fichoni kwake alioko huko juu, alalaye kivulini kwake aliye Mwenyezi humwambia Bwana: Kimbilio langu, tena ngome yangu, Mungu wangu, nimwegemeaye! Kwani yeye ndiye aniokoaye tanzini mwa mwindaji, namo mwenye kipindupindu kiangamizacho. Kwa manyoya yake atakufunika, namo mabawani mwake ndani utakimbilia, welekevu wake ni ngao, hata kingio. Hutaogopa mastusho ya usiku, wala mshale upigwao mchana, wala kipindupindu kinyatiacho gizani, wala magonjwa mengine mabaya yauayo na mchana. Kama wataanguka elfu zima upande wako, au maelfu kumi kuumeni kwako, lakini kwako wewe hayatafika. Kweli, macho yako yenyewe yatavitazama; jinsi wasiomcha Mungu wanavyolipishwa, utaviona. Kwani wewe ulisema: Bwana ni kimbilio langu, naye Alioko huko juu unamtumia kuwa kao lako. Hakuna kibaya kitakachokufikia mwako nyumbani, wala hakuna pigo litakalokikaribia kituo chako. Kwani atakuagizia malaika zake, wakulinde katika njia zako ziwazo zote. Nao watakuchukua mikononi mwao, usije kujikwaa mguu wako katika jiwe. Utakanyaga simba nao nyoka, utaponda kwa mateke wana wa simba nao nondo. Kwa kuwa ameshikamana na mimi, nitamwopoa, kwa kuwa analijua Jina langu, nitamkweza. Atakaponiita, nitamwitikia, mimi niko pamoja naye katika masongano, nimwokoe, kisha nimpe hata utukufu. Wingi wa siku zake za kuwapo ndio, nitakaomshibisha, nimchangamshe, akiuona huo wokovu wangu. Ni kitu kizuri kumshukuru Bwana na kuliimbia Jina lako, ulioko huko juu, asubuhi kuutangaza upole wako, tena usiku welekevu wako kwa kupiga mapango yenye nyuzi kumi pamoja na mazeze yaliayo vizuri. Kwani, wewe Bwana, umenifurahisha kwa matendo yako, kazi za mikono yako ninazishangilia. Kazi zako, Bwana, ni kubwa peke yao, mawazo yako ni marefu mno, hayachunguziki. Lakini mtu asiyejua kitu hayatambui, wala mpumbavu hayaoni hayo. Wasiomcha Mungu wakichipuka kama majani, nao wote wafanyao maovu wakichanua vizuri, ni kwamba tu: Sharti waangamizwe kale na kale. Wewe, Bwana, unatukuka kale na kale. Kwani, Bwana, ukiwatazama wao wachukivu wako, ukiwatazama vema wao wachukivu wako, mara hupotea, wote wafanyao maovu hutawanyika. Lakini baragumu langu umelielekeza juu kama pembe za nyati, nikafurikiwa na mafuta ya mwaka huu. Macho yangu yataona furaha kwao walioninyatia, masikio yangu yatayasikia na kiyafurahia, wabaya walioniinukia waliyofanyiziwa. Mwongofu atachipuka kama mtende, atakua kama mwangati ulioko Libanoni. Kwenye Nyumba ya Bwana wako wlaiopandwa huko, watachipuza matawi katika nyua zake Mungu wetu; ijapo, wawe wazee, wataendelea kuzaa, maana watakuwa wenye utomvu na majani mengi. Hivyo watautangaza unyofu, Bwana alio nao; mwake yeye aliye mwamba wangu hamna upotovu. *Bwana ni mfalme, huvaa yenye urembo; kweli Bwana huvaa, nayo nguvu ndiyo, aliyojifunga kiunoni. Hivyo ndivyo, alivyoishikiza nchi, isije kuyumbayumba. Kiti chake cha kifalme kimeshikizwa na nguvu tangu mwanzo, tangu kale na kale wewe upo. Bwana, huzivumisha sauti zao mito mikubwa, kweli mito mikubwa huzivumisha sauti zao, huvivumisha vishindo vyao hiyo mito mikubwa. Lakini nguvu za mavumi ya hayo mafuriko ya maji yaliyo mengi, hata nguvu za mawimbi ya bahari yaumukayo zinapitwa na nguvu zake Bwana atukukaye. Mashuhuda yako hutegemeka sana, pambo liipasalo Nyumba yako, Bwana, ndio utakatifu, nao utakuwako siku zote zitakazokuwa.* Bwana uliye Mungu mwenye lipizi, Mungu uliye mwenye lipizi, tokea! Wewe uliyeiamulia nchi, inuka! Warudishie wenye majivuno matendo yao! Wasiokucha, Bwana, wakubeze mpaka lini? Hao wasiokucha waseme makuu yao mpaka lini? Wanazidi kusimuliana na kusema makorofi, wote wafanyao maovu hujisemea hivyo. Walio ukoo wako huwaponda, walio fungu lako huwatesa; wajane na wageni huwanyonga, wafiwao na wazazi huwaua. Bwana havitazami! Ndivyo, wanavyosema, Mungu wa Yakobo havitambui! Vitambueni, ninyi msiojua kitu, mlio wa ukoo wetu! Nanyi wajinga, mtaerevuka lini? Aliyelifanya sikio, asisikie? Aliyeliumba jicho, asione? Achapuaye wamizimu, asipatilize? Siye yeye afundishaye watu, wapate kujua? Lakini Bwana huyatambua mawazo ya watu, ya kuwa hayo ndiyo yaliyo ya bure. Mwenye shangwe ni mtu, umchapuaye, wewe Bwana, na kumfundisha yaliyomo katika Maonyo yako, ayajue. Hivyo atajituliza kwa kuona, siku za wabaya zilivyo, mpaka wasiokucha wachimbiwe mashimo. Kwani Bwana hatawatupa walio ukoo wake, nao walio fungu lake hatawaacha. Kwani pako bado, watu wanapoamuliwa kwa wongofu wote wenye mioyo inyokayo watapafuata hapohapo. Yuko nani atakayeinuka kuwa upande wangu, nikipigana nao wabaya? Yuko nani atakayesimama kwangu, nikipigana nao wafanyao maovu? Kama Bwana asingekuwa anisaidiaye, roho yangu ingekuwa imekwisha kulala mahali palipo kimya. Niliposema moyoni: Mguu wangu umejikwaa, ndipo, upole wako, Bwana, uliponishikiza. Mawazo yalipozidi kuwa mengi moyoni mwangu, ndipo, matulizo yako yalipoichangamsha roho yangu. Je? Wewe uko na bia napo panapoamuliwa kwa ukorofi? Maana ndipo panapoleta maumivu kwa kuyapotoa yaliyo ya kweli. Wao huishambulia roho yake aliye mwongofu, humwaga damu zao wasiokosa. Lakini Bwana ndiye atakayekuwa ngome yangu, yeye Mungu ni mwamba wangu wa kuukimbilia. Atawalipiza mapotovu yao na kuwamaliza kwa ubaya wao, Bwana Mungu wetu atawamaliza kweli. Njoni, tumpigie vigelegele yeye Bwana! Aliye mwamba wa wokovu wetu na tumshangilie! Na tumtokee usoni pake na kumshukuru! Na tumshangilie na kumwimbia! Kwani Bwana ndiye Mungu aliye mkuu, ni mfalme mkuu kuliko miungu yote. Kwani mkononi mwake vimo vilivyomo ndani ya nchi, vileleni kwa milima nako ndiko kwake. Bahari ni yake, maana ndiye aliyeifanya, mikono yake iliziumba nazo hizo nchi kavu. Njoni, tumtambikie na kumwangukia! Na tupige magoti mbele yake Bwana aliyetufanya! Kwani yeye ni Mungu wetu, nasi watu wake, hutuchunga kwa kuwa kondoo waliomo mkononi mwake. Leo mtakapoisikia sauti yake, msiishupaze mioyo yenu, kama vilivyokuwa kule Meriba au Masa, mlipokuwa kule nyikani. Ndipo, baba zenu waliponijaribu na kunipima, tena walikuwa wameyaona matendo yangu. Nikachafuliwa moyo miaka arobaini nao wa kizazi hicho, nikasema: Wao ndio watu walioipoteza mioyo yao, nao ndio waliokataa kuzitambua njia zangu. Kwa hiyo nilijiapia kwa makali yangu: Hawataingia kamwe kwenye kituo changu! *Mwimbieni Bwana wimbo mpya! Mwimbieni Bwana, nchi zote! Mwimbieni Bwana! Likuzeni Jina lake! Utangazeni wokovu wake siku kwa siku! Wasimulieni wamizimu utukufu wake nako kwenye makabila yote ya watu mataajabu yake! Kwani mkuu ni Bwana, apaswa na kutukuzwa sana, naye anaogopesha kuliko miungu yote. Kwani miungu yote ya makabila ya watu ni ya bure tu, lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu. Ukuu na urembo uko mbele yake, uwezo na utukufu upo Patakatifu pake. Ninyi mlio wa ukoo wa watu, mpeni Bwana yaliyo yake! Kwa kuwa ni mtukufu na mnguvu, mpeni Bwana yaliyo yake! Kwa kuwa jina lake ni tukufu, mpeni Bwana yaliyo yake! Chukueni vipaji vya tambiko, mje kuziingia nyua zake! Mtambikieni Bwana na kuvaa mapambo yapasayo Patakatifu! Mkimtokea, mastuko na yawaguie, ninyi wa nchi zote! Tangazeni kwa wamizimu kwamba: Bwana ni mfalme! Yeye ndiye aliyeishikiza nchi, isije kuyumbayumba, yeye ndiye atakayewaamulia watu maamuzi yanyokayo.* Kwa hiyo mbingu na zifurahi, nchi nayo na ipige shangwe! Hata bahari nayo yote yajaayo ndani yake na yavume! Mashamba nayo yote yaliyomo na yapige vigelegele! Itakuwa, nayo miti yote ya mwituni imshangilie Bwana, kwani ndiye atakayekuja kweli kuihukumu nchi, atauhukumu ulimwengu kwa wongofu, nayo makabila ya watu kwa welekevu wake. Bwana ni mfalme! Nchi na zishangilie! Navyo visiwa vilivyo vingi na vifurahi! Mawingu yenye giza yanamzunguka, shikizo la kiti chake cha kifalme ni wongofu unyoshao maamuzi. Moto ndio unaomtangulia, nao unawateketeza wabishi wake po pote, walipo. Meme, azipigazo, zinamulika huku nchini, nazo nchi hustuka zikiziona. Milima inayeyuka kama nta mbele yake Bwana, mbele yake yeye azitawalaye nchi zote. Mbingu zinautangaza wongofu wake, nayo makabila yote ya watu huuona utukufu wake. Sharti wapatwe na soni wote watumikiao vinyago, wajivuniao miungu iliyo ya bure; mwangukieni yeye, ninyi miungu yote! Wasioni wanavisikia na kufurahi, binti Yuda hukupigia vigelegele, Bwana, kwa ajili ya maamuzi yako, Kwani wewe Bwana ndiwe uliye mkuu wa ulimwengu wote, wewe unatukuka sana kuliko miungu yote. Ninyi mmpendao Bwana, yachukieni mabaya! Huzilinda roho zao wamchao yeye, huwaopoa mikononi mwao wasiomcha Mungu. Mwanga unamzukia aliye mwongofu, nayo furaha inawazukia walionyoka mioyo. Ninyi waongofu, mfurahieni Bwana, mwakumbushe watu utakatifu wake! Mwimbieni Bwana wimbo mpya! Kwani hufanya mataajabu. Mkono wake wa kuume humpatia kushinda. maana huo mkono wake ni wenye utakatifu. Bwana huujulisha wokovu wake, machoni pao wamizimu huufunua wongofu wake. Huukumbuka upole na welekevu wake, aliouagia mlango wa Isiraeli, mapeo yote ya nchi yameuona wokovu wa Mungu wetu. Mpigieni Bwana shangwe, nchi zote! Pazeni sauti! Shangilieni na kumwimbia! Mwimbieni Bwana na kupiga mazeze, mazeze yakizifuata sauti za nyimbo! Pigeni mabaragumu yenye kulia sana mkishangilia mbele yake bwana, ya kuwa ni mfalme! Bahari na ivume nayo yote yaliyomo! Hata nchi pamoja nao wakaao humo! Mito mikubwa na iitikie na milima pamoja, yote na ishangilie! Bwana atakapokuja ataihukumu nchi, atauhukumu ulimwengu kwa wongofu nayo makabila ya watu kwa unyofu.* Bwana ni mfalme, kwa hiyo makabila ya watu hutetemeka. Yeye anakaa juu ya Makerubi, lakini nchi inayumbayumba. Bwana ni mkuu mle Sioni, anayapita makabila yote ya watu kwa kutukuka. Na walishukuru Jina lako kubwa lililo la kuogopesha; aliye mtakatifu ndiye yeye. Nguvu za mfalme huyu ni kupenda maamuzi yaliyo sawa. Wewe ndiwe uliyetoa unyofu wa kuyashikiza, nawe ndiwe uliyeamua kwa Yakobo maamuzi yaongokayo. Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu! Hapo, anapoiwekea miguu yake, mwangukieni! Aliye mtakatifu ndiye yeye. Mose na Haroni walikuwa miongoni mwao watambikaji wake, Samueli alikuwa miongoni mwao waliolililia Jina lake. Alisema nao akiwa amejificha katika wingu lililokuwa kama nguzo, wao wakayashika maneno, aliyowashuhudia, hata maagizo, aliyowapa. Bwana, wewe ndiwe Mungu wetu. uliwaitikia kwa kuwa Mungu wao aondoaye makosa, tena kwa ajili ya matendo yao ukawalipiza. Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu! Mwangukieni mlimani kwenye utakatifu wake! Kwani Bwana Mungu wetu ni mtakatifu. Mpigieni Bwana shangwe, nchi zote! Mtumikieni Bwana na kufurahi! Tokeeni mbele yake na kupiga shangwe! Tambueni, ya kuwa aliye Mungu ndiye yeye Bwana! Yeye ndiye aliyetufanya, sio sisi wenyewe, tu watu wa ukoo wake na kondoo wa malishoni pake. Ingieni milangoni mwake na kumshukuru! Ziingieni nyua zake na kumshangilia! Mshukuruni! Nalo Jina lake likuzeni sana! Kwani Bwana ni mwema, nao upole wake ni wa kale na kale, nao welekevu wake ni wa vizazi na vizazi. Upole na uamuzi wa kweli nitauimbia, nitakutungia wimbo, wewe Bwana. Nitajitafutia ujuzi wa kuifuata njia iliyo yenye kweli yote. Itakuwa lini, ukija kwangu? Nitaendelea kuutakasa moyo wangu humu nyumbani mwangu. Sitayaelekeza macho yangu kwenye mambo yasiyofaa, nachukizwa na kufanya mapotevu, hayagandamani na mimi. Moyo ulio wenye upotovu sharti uondoke kwangu, sitaki kulijua lililo baya. Amsingiziaye mwenziwe kinjamanjama ndiye, nitakayemmaliza, mwenye macho makuu na mwenye moyo wa kujivuna simvumilii. Macho yangu huwatazama walio welekevu katika nchi, wakae kwangu, naye aifuataye njia yenye kweli yote ndiye atakayenitumikia. Afanyae udanganyifu hakai nyumbani mwangu, wala asemaye uwongo hatasimama machoni pangu. Kila kunapokucha nitawamaliza katika nchi wote wasiomcha Mungu, nao wote wafanyao maovu nitawang'oa mjini mwake Bwana. Maombo ya mnyonge; kwa kufikisha kuzimia roho anamtolea Bwana wasiwasi wake. Bwana, lisikilize ombo langu! Kilio changu sharti kifike kwako wewe. Usiufiche uso wako, nisiuone ninaposongeka! Nitegee sikio lako, ninapokuita, uniitikie upesi! Kwani siku zangu hupotea kama moshi, nayo mifupa yangu huchomwa kama vijinga vya moto. Moyo wangu umeungua, ukanyauka kama majani, kwa hiyo mimi husahau kula chakula changu. Kwa hivyo, ninavyolia na kupiga kite, nyama za mwili wangu zimegandamana nayo mifupa. Nimefanana na korwa wa huko jangwani, nikawa kama bundi akaaye mahameni. Ninalala macho kwa kulia, ninafanana na ndege aliyeachwa peke yake kipaani juu. Siku zote adui zangu hunisimanga, hunizomea na kuapa, nipatwe na mabaya. Kwani ninakula uvumbi, kama ni mkate, navyo vinywaji vyangu ninavichanganya na machozi, kwa sababu umenitolea makali na kunichafukia, kisha ukanikamata, ukanibwaga. Siku zangu ni kama kivuli kilicho kirefu, nami nimenyauka kama majani. Lakini wewe, Bwana, utakaa kale na kale, kwa vizazi na vizazi utakumbukwa. Wewe utakapoinuka, uhurumie Sioni! Kwani siku za kuuonea uchungu sasa ziko, kweli imekwisha kufika saa yake. Kwani watumishi wako hupendezwa, mawe yake yakitumiwa; tena jinsi yanavyokaa uvumbini, inawatia uchungu. Ndipo, wamizimu watakapoliogopa Jina lake Bwana, nao wafalme wote wa nchi watauogopa utukufu wako. Hapo, Bwana atakapokuwa ameujenga tena mji wa Sioni, ndipo, utakapokuwa umetokea nao utukufu wake. Atayageukia maombo yao walio wakiwa, maana yale maombo yao hakuyabeza. Hayo sharti yaandikiwe vizazi vitakavyozaliwa nyuma, nao wa ukoo utakaoumbwa sharti wamshangilie Bwana. Kwani alichungua toka Patakatifu pake palipo juu toka mbinguni aliitazama nchi hii, awasikilize waliofungwa, wakimpigia kite, nao walio wana wa kifo awafungulie njia, wapate kulitangaza mle Sioni Jina lake Bwana pamoja na kumshangilia mlemle Yerusalemu, makabila ya watu yatakapokusanyika yote pia pamoja na wafalme, wamtumikie Bwana. Njiani alizipunguza nguvu zangu, nazo siku zangu akazifupiza. Nikasema: Mungu wangu, usiniondoe, siku zangu simefika kati tu! Miaka ikaayo kwa vizazi na vizazi ni yako wewe. Huko kale uliiweka misingi ya nchi, mbingu nazo ni kazi ya mikono yako wewe. Hizo zitaangamia, lakini wewe utasimama. Kweli, zote zitachakaa kama nguo; utakapozigeuza kama vazi, ndipo, zitakapogeuka. Lakini wewe ndiwe yuleyule uliyekuwa kale, miaka yako haitakoma. Wana wa watumishi wako watakaa nao, nao wa uzao wao watakaa usoni pako wakiwa wenye nguvu. Mtukuze Bwana, roho yangu! Navyo vyote vilivyomo ndani yangu mimi na vilitukuze Jina lake lililo takatifu! Mtukuze Bwana, roho yangu! Usiyasahau mema yote, aliyokutendea! Alikuondolea manza zote, ulizozikora, nayo magonjwa yako yote akayaponya. Akazikomboa roho zako kuzimuni, kisha akakufunga kilemba, ndio magawio ya upole. Amekushibisha mema, yawe urembo wako; ujana wako ukarudi kuwa mpya kama ule wa kozi. Bwana hufanya yenye wongofu na kuwaamulia wote wakorofikao. Alimjulisha Mose njia zake, wana wa Isiraeli aliwajulisha matendo yake. Bwana ni mwenye huruma na mwenye utu, tena ni mwenye uvumilivu na mwenye upole mwingi. Hatagomba kale na kale, wala hatayashika makali siku zote. Hatatufanyizia yapasayo makosa yetu, wala hatatulipisha manza, tulizozikora. Kwani kama mbingu zinavyokuwa juu ya nchi, ndivyo, upole wake unavyokua kwao wamwogopao. Kama maawioni na machweoni kunavyokaliana mbali, ndivyo, alivyoyaweka maovu yetu, yatukalie mbali. Kama baba anavyowaonea uchungu walio wanawe, ndivyo, Bwana anavyowaonea uchungu wao wamwogopao. Kwani yeye anajua, jinsi alivyotuumba, hukumbuka, ya kuwa sisi tu mavumbi. Mtu siku zake hufanana nayo majani, huchanua kama ua la porini; lakini upepo ukipita juu yake, haliko tena, wala watu hawapatambui tena mahali, lilipokuwa. Lakini upole wake Bwana huwakalia wamwogopao tangu kale hata kale, nao wongofu wake huwakalia wana kwa wana kwao walishikao Agano lake na kuliangalia nako kwao wayakumbukao maagizo yake, wayafanye. Bwana alikisimamaisha mbinguni kiti chake cha kifalme, ufalme wake unawatawala watu wote pia. Mtukuzeni Bwana, ninyi malaika zake! Nanyi wakuu wa vikosi mlio wenye nguvu, mlifanyao Neno lake, mkilisikiliza hilo Neno lake, sauti yake ikitokea! Mtukuzeni Bwana, ninyi vikosi vyake vyote! Nanyi watumishi wake myafanyao yampendezayo! Mtukuzeni Bwana, matendo yake yote mahali po pote, anapotawala! Mtukuze Bwana, roho yangu! Mtukuze Bwana, roho yangu! Bwana Mungu wangu, u mkuu kabisa, yenye urembo na utukufu umeyavaa. Umejivika mwanga, kama ni kanzu, ukazitanda mbingu kama nguo za hema. Makao yake ya juu aliyawekea misingi ya majini, huyatumia mawingu kuwa gari lake, juu ya mabawa ya upepo hujiendea. Huwatumia malaika zake kuwa upepo, nao watumishi wake kuwa mioto iwakayo. Aliishikiza nchi kwenye misingi yake, haitayumbayumba kale na kale; ukaivika vilindi vya maji, kama ni nguo, nako vileleni kwenye milima juu kulikuwa na maji, nayo yalikuwa yametulia kuko huko. Ulipoyakemea, yakakimbia, ulipoyapigia sauti za ngurumo, yakapiga mbio kujiendea. Milima ikainukia kwendelea juu, mabonde yakatelemkia hapohapo, ulipoyatengenezea. Ukakata mipaka, maji yasiipite, yasirudi tena kuifunika nchi. Namo mabondeni ukatokeza chemchemi za maji, maji yapate kupita katikati ya milima. Nyama wote wa porini wakapata ya kunywa hukomesha kiu humo akina punda milia. Nao ndege wa angani hukaa kando ya maji, hupiga nyimbo zao wakikaa katika matawi ya miti. Milima ukainywesha maji yatokayo juu, ukaishibisha nchi mapato ya kazi zako. Ukachipuza majani, nyama wapate kula, nayo maboga, watu wayatumie; ndivyo, ulivyovitoa vilaji huku mchangani, hata mvinyo zifurahishazo mioyo ya watu, nayo mafuta ya kuzing'aza nyuso zao, nayo mikate itiayo nguvu mioyoni mwa watu. Hata miti ya Bwana hunywa, mpaka ishibe, kama miangati ya Libanoni, aliyoipanda yeye. Ndimo, ndege wanamojenga viota vyao, nazo nyumba zao makorongo ziko katika mivinje. Kwenye milima mikubwa ndiko, minde wanakokaa, magenge ni kimbilio lao wale pelele. Uliumba mwezi wa kujulisha vilimo, jua hupajua pake pa kuchwea. Ukaiweka nayo giza, usiku uwepo; ndipo, nyama wa porini wanapotembea wote, wana wa simba hunguruma wakikosa nyama wa kukamata; ndivyo, wanavyomwuliza Mungu chakula chao. Jua linapokucha, wale hurudi kwao mapangoni mwao, wapate kulala. Kisha hutokea watu kwenda kazini, watumikie huko kazini mpaka jioni. Uliyoyafanya, Bwana, ni makuu, tena ni mengi! Yote pia uliyafanya kwa ubingwa ulio wa kweli, hivyo nchi ikapata kijana viumbe vyako. Hapo ni bahari iliyo kubwa na pana pande zote; humo ndimo, wanamofurika wadudu wasiohesabika kabisa, tena nyama wadogo nao wakubwa. Humo zinapita nazo merikebu zenye mizigo, tena wamo nondo, uliowaumba wa kuchezea mle. Hawa wote wanakuelekea wakikutazamia, uwape vilaji vyao, wanapoona njaa. Ukiwapa, hukusanya, tena hulimbika, unapokifumbua kiganja chako, hushiba mema yako. Ukiuficha uso wako, wataguiwa na kituko, ukiondoa pumzi zao, huzimia, kisha hurudi uvumbini. Unapoituma pumzi yako, wanaumbwa, nao uso wa nchi huurudishia upya. Utukufu wake Bwana ni wa kale na kale, naye Bwana huzifurahia kazi, alizozifanya. Akiitazama nchi, inatetemeka; akiigusa milima, inatoka moshi. Siku zangu zote za kuwapo nitamwimbia Bwana, nitampigia Mungu wangu shangwe nikingali nipo. Nyimbo zangu, nilizozitunga, na zimpendeze! Mimi ninayemfurahia, ndiye Bwana. Wakosaji sharti wamalizwe, wasiwepo nchini tean! Mtukuze Bwana, roho yangu! Haleluya! Mshukuruni Bwana, nalo Jina lake litambikieni! Yajulisheni makabila ya watu matendo yake! Mpigieni shangwe za kumwimbia! Mataajabu yake yote yatungieni tenzi! Lishangilieni Jina lake lililo takatifu! Mioyo yao wamtafutao Bwana na ifurahi! Mchungulieni Bwana nazo nguvu zake! Utafuteni uso wake siku zote! Yakumbukeni mataajabu yake, aliyoyafanya, nayo maamuzi yake yashangazayo yakisemwa na kinywa chake! Ninyi mlio wa uzao wake Aburahamu aliyemtumikia, nanyi wana wa Yakobo, yeye aliyemchagua! Yeye Bwana ni Mungu wetu, nchi zote anaziamua. Kale na kale analikumbuka Agano lake. aliowaagiza kulishika Neno lake, ni vizazi elfu. Agano ni lile, alilomwekea Aburahamu, nacho kiapo ni kile, alichomwapia Isaka. Mbele yake Yakobo naye akalisimamisha kuwa maongozi, Agano lakale na kale liwe kwake Isiraeli kwamba: Wewe ndiwe, nitakayekupa nchi ya Kanaani, iwe fungu lenu, nililowapimia. Vilikuwa hapo, walipokuwa kikundi cha watu wanaohesabika, maana kule walikuwa wachache tu, tena wageni. Wakawaendea watu wa huko, taifa kwa taifa, walipotoka kwa mfalme mmoja, wakawajia wenziwe. Lakini hakuna mtu, aliyempa ruhusa kuwakorofisha, hata wafalme akawapatiliza kwa ajili yao kwamba: Niliowapaka mafuta msiwaguse tu, wala wafumbuaji wangu msiwafanyizie mabaya! Akaita njaa, ije kuziingia nchi za watu, akaivunja miti yote izaayo vilaji. Hapo alikuwa amekwisha kujipatia mtu, awafungulie njia, ni Yosefu aliyekuwa ameuzwa kuwa mtumwa. Huyo miguu yake waliiumiza kwa kuitia katika mapingu, kisha wakamfunga mwenyewe kwa minyororo mpaka siku ile, lilipotimia lile neno lake; naye alikuwa ameng'azwa kwa kuyeyushwa na maneno yake Bwana. Ndipo, mfalme alipotuma, akamfungua; mtawala makabila ya watu akamtoa kifungoni. Akamsimamisha kuwa bwana nyumbani mwake na mtunzaji wa mali, alizokuwa nazo zote, awafunge wakuu wake, kama apendavyo; kisha awafundishe wazee wake, waerevuke. Ndipo, Waisiraeli walipokuja huko Misri, Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu. Bwana akawapa wao walio ukoo wake kuzaa sana, akawatia nguvu kuliko wao waliowasonga. Kisha akaigeuza mioyo yao wale, wawachukize walio ukoo wake, wakawaendea watumishi wake kwa udanganyifu. Ndipo, alipomtuma mtumishi wake, yule Mose, naye Haroni, aliyemchagua. Hao wakafanya kwao vielekezo, alivyokuwa aliwaambia, wakavifanya vioja vyake katika nchi ya Hamu. Akatuma giza, likaiguia nchi yao, nao hawakukataa kuyatii maneno yake. Akayageuza maji yao kuwa damu. akawaua nyama wote wa humo mtoni. Nchi yao ikafurikiwa navyo vyura, wakaingia namo nyumbani mwa mfalme wao. Mbung'o wakaja papo hapo, aliposema, katika mipaka yao yote wakaingia nao mbu. Penya mvua zao aliwanyeshea mvua ya mawe pamoja na mioto iliyoichoma nchi yao. Akaipiga mizabibu yao, hata mikuyu yao, akaiponda miti iliyokuwako katika mipaka yao. Nzige wakaja papo hapo, aliposema, pamoja na funutu wasiohesabika. Wakala majani yote katika nchi yao. wakala navyo vilaji vyote mashambani kwao. Akampiga kila mzaliwa wa kwanza katika nchi yao, ndio wote waliokuwa malimbuko yenye nguvu kwao. Alipokwisha kuwapatia fedha na dhahabu, ndipo, alipowatoa, tena katika koo zao hakuwamo aliye mwenye kilema. Wamisri wakafurahi, walipotoka, kwani waliguiwa na kituko kilichowaogopesha. Akatanda wingu, liwafunike, kisha liwe lenye moto, uwamulikie usiku. Walipomwomba, akaleta tombo, hata mikate alitoa mbinguni, akawashibisha. Akafungua mwamba, maji yakabubujika, yakajiendea nyikani kama mto. Kwani alilikumbuka Neno lake lililo takatifu, alilomwambia mtumishi wake Aburahamu. Ndivyo, alivyowatoa walio ukoo wake, wakafurahi, kwa kuwa wateule wake wakampigia vigelegele. Nchi zao wamizimu ndizo, alizowapa, navyo, makabila mengine yalivyovisumbukia, wakavitwaa tu. Alitaka hili tu: Wayaangalie maongozi yake, nayo Maonyo yake wayashike. Haleluya! Haleluya! Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema! Ya kuwa upole wake ni wa kale na kale! Yuko nani atakayemaliza kuyasimulia matendo ya nguvu ya Bwana? Yuko nani tena atakayeyatanganza matukuzo yake yote? Wenye shangwe ndio wayashikao yanyokayo nao wafanyao siku zote yaliyo yenye wongofu. Bwana, nikumbuke kwa kupendezwa nao walio ukoo wako! Unijie kunikagua, upate kuniokoa, nami nipate kuyatazama mema yao wateule wako, tena niifurahie furaha yao walio kabila lako, tushangilie pamoja nao walio fungu lako! Pamoja na baba zetu tulikosa nasi, tulipoacha kumcha Mungu tulikora manza. Baba zetu walipokuwako kule Misri, walipoyaona mataajabu yako hawakuerevuka, hawakuyakumbuka yale mema mengi, uliyawagawia, wakakataa kukutii kule baharini, kwenye Bahari Nyekundu. Lakini kwa ajili ya Jina lake aliwaokoa, awajulishe uweze wake wenye nguvu. Akaikaripia Bahari Nyekundu; ndipo, ilipokupwa, akawapitisha kule vilindini, kama ni nyikani. Akawaokoa mikononi mwao waliowachukia, akawakomboa mikononi mwao waliokuwa adui zao. Maji yakawafunika wao waliowasonga, kwao hakusalia hata mmoja. Ndipo, walipoyategemea maneno yake, wakamwimbia mashangilio ya kumsifu. Lakini upesi sana wakayasahau matendo yake, aliyoyataka kuwaeleza hawakuyangojea. Walipoingiwa na tamaa kule nyikani wakazifuata, wakamjaribu Mungu huko jangwani. Akawapa waliyomwomba, akayafurikisha, mpaka yakizichafua roho zao. Kisha wakamwonea Mose wivu hapo, walipopanga, hata Haroni aliyekuwa mtakatifu wake Bwana. Nchi ikaasama, ikammeza Datani, ikawafunika nao akina Abiramu. Moto ukawaka kwenye mkutano wao, ndimi zake zikawateketeza wasiomcha Mungu. Wakafanya ndama kule Horebu, wakakitambikia hicho kinyago. Hivyo ndivyo, walivyougeuza utukufu wao kuwa kama wa ng'ombe mwenye kula majani. Wakamsahau Mungu aliyewaokoa na kufanya mambo makuu kule Misri. Nayo yaliwastaajabisha walioko katika nchi ya Hamu, nako kwenye Bahari Nyekundu yakawastusha. Akawaza kuwamaliza, waishe kabisa, kama Mose, aliyemchagua, asingalijisimamisha mbele yake kwenye ule ufa ulioatuka, ayatulize machafuko yake, asiwaangamize. Wakaibeza ile nchi iliyo nzuri zaidi. hawakulitegemea Neno lake. Katika mahema yao wakanung'unika, hawakuisikiliza sauti yake yeye Bwana. Akauinua mkono wake, awapige, awaue nyikani, awatapanye walio wa uzao wao kwenye wamizimu na kuwamwaga katika nchi zilizokuwa za wengine. Kisha wakaja kugandamana na Baali Peori, wakala nyama za tambiko la mizimu; Ndivyo, walivyomkasirisha na matendo yao. Kisha kilipotukia kwao kipindupindu, ndipo, Pinehasi alipotokea, akawaonya, nacho kipindupindu kikazuiliwa papo hapo. Kwa hivyo aliwaziwa kuwa mwenye wongofu kwa vizazi na vizazi kale na kale. Kisha wakamchafua moyo tena kwenye maji ya Meriba, Mose naye akapatwa na mabaya kwa ajili yao. Kwani walipoibishia roho yake, midomo yake ilisema maneno yasiyompasa. Kisha hawakuyamaliza makabila ya watu. Bwana aliyowaagiza kuwaua. Ila walichanganyika nao wamizimu, nayo matendo yao wakayaiga. Navyo vinyago vyao wakavitumikia, navyo ndivyo vilivyowanasa. Wana wao wa kiume nao wa kike wakawatoa kuwa ng'ombe za tambiko za mizimu. Nazo damu zisizokuwa zenye manza wakazimwaga, ni damu za wana wao wa kiume na wa kike, waliowatoa kuwa ng'ombe za tambiko za vinyago vya Kanaani; ndivyo, walivyoichafua nchi kwa kumwaga damu. Hata wenyewe walijichafua kwa hayo matendo yao, kwa kuzifanya hizo kazi zao wakawa wagoni. Ndivyo, walio ukoo wake walivyokoleza moto wa makali yake Bwana, wao waliokuwa fungu lake wakamtapisha, akawatia mikononi mwao wamizimu, walio wachukivu wao wakawatawala. Adui zao wakawatesa, wakashurutishwa kuiinamia mikono yao. Mara nyingi aliwaopoa, lakini kwa mashauri yao wakamkataa, wakabanwa kwa ajili ya manza, walizozikora. Kisha akawatazama, jinsi walivyosongeka; alipoyasikia malalamiko yao, yalipoingia masikioni mwake, akalikumbuka Agano lake, alilolifanya nao, kwa upole wake mwingi akawahurumia, akawapatia huruma kwao wote waliowafunga. Tuokoe, Bwana, uliye Mungu wetu! Tukusanye na kututoa kwenye wamizimu, tupate kulishukuru Jina lako takatifu, tuzidishe kukusifu na kukushangilia! Na utukuzwe, Bwana Mungu wa Isiraeli, tangu kale hata kale! Nayo makabila yote ya watu sharti yaitikie: Amin! Haleluya! Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema! Ya kuwa upoke wake ni wa kale na kale! Ndivyo, watakavyosema waliokombolewa na Bwana, aliowakomboa katika masongano. Ndio, aliowakusanya na kuwatoa katika nchi za ugeni, kule maawioni kwa jua nako macheoni kwake, nako kaskazini nako kwenye bahari. Walikuwa wamepotea nyikani katika njia za jangwani, mji uliokuwa wenye watu hawakuuona. Njaa ikawauma pamoja na kiu, roho zao zikataka kuzimia tu. Ndipo, walipomlilia Bwana kwa kusongeka hivyo, naye akawaopoa katika masumbuko yao. Akawaongoza katika njia iliyonyoka, wapate kufika mjini mwenye watu. Hao na wamshukuru Bwana, ya kuwa ni mpole! Huwafanyizia wana wa watu vioja vyake, hushibisha roho yenye kiu, nayo roho yenye njaa huipatia mema mengi. Wako wengine, walikaa gizani mwenye kufa, wakawa wamefungwa na kubanwa na vyuma. Kwani walikataa kuyatii maneno yake Mungu, wakalibeza shauri lake yule Alioko huko juu. Kwa hiyo aliinyenyekeza mioyo yao kwa kuwatesa, nao walipojikwaa, hakuwako aliyewasaidia. Ndipo, walipomlilia Bwana kwa kusongeka hivyo, naye akawaokoa katika masumbuko yao. Akawatoa gizani mwenye kufa, yale mafungo yao nayo akayavunja. Hao na wamshukuru Bwana, ya kuwa ni mpole! Huwafanyizia wana wa watu vioja vyake. Kwani milango ya shaba anaivunja, nayo makomeo ya chuma anayakata. Wako wengine waliopumbazwa na kuumizwa kwa ajili ya njia zao zenye mapotovu na kwa ajili ya kukora manza. Vilaji vyote vikazichafua roho zao, mwisho wakajifikisha huko, malango ya kifo yaliko. Ndipo, walipomlilia Bwana kwa kusongeka hivyo, naye akawaokoa katika masumbuko yao. Akalituma Neno lake, likawaponya, akawaopoa shimoni mwao. Hao na wamshukuru Bwana, ya kuwa ni mpole! Huwafanyizia wana wa watu vioja vyake. Na wamtolee vipaji vya tambiko vya kumshukuru wakiyasimulia matendo yake na kushangilia. Wako wengine waliosafiri baharini katika merikebu wakifuata uchuuzi kule kwenye maji mengi. Nao waliyaona matendo ya Bwana na vioja vyake kwenye vilindi. Kwa kusema tu alileta upepo wa kimbunga uliokweza mawimbi, yakawapandisha juu kwenda mbinguni, tena wakatelemka chini vilindini, roho zao zikayeyuka kwa hayo mabaya. Wakayumbayumba na kupepesuka kama mlevi, mizungu yao yote ikawa ya bure. Ndipo, walipomlilia Bwana kwa kusongeka hivyo, naye akawatoa katika masumbuko yao. Akakituliza kimbunga, kukawa kimya, mawimbi nayo yakanyamaza. Kwa kuwa yamepata kutulia, wakafurahi, kisha akawaingiza bandarini, walikotaka kwenda. Hao na wamshukuru Bwana, ya kuwa ni mpole! Huwafanyizia wana wa watu vioja vyake. Na wamtukuze kwenye mikutano ya watu walio wa ukoo wetu! Nako kwenye mashauri ya wazee na wamshangilie! Aligeuza mito mikubwa kuwa nyika, nazo mboji za maji kuwa nchi kavu. Nchi yenye wiva akaigeuza kuwa jangwa la chumvi kwa ajili ya ubaya wao waliokaa kule. Tena nyika aliigeuza kuwa bwawa lenye maji mengi, nayo nchi kavu akaitokeza mboji za maji, akawapa wenye njaa ya kukaa hapohapo, wapajengee mji wa kukaa. Wakalima mashamba, wakapanda mizabibu, wakajipatiamo matunda, ndio malipo ya kazi zao. Kwa hivyo, alivyowabariki, wakawa wengi sana, nao nyama wa kufuga, aliowapa, hawakuwa wachache. Kisha wakapunguka tena, wakainamishwa chini kwa kulemewa na mabaya yaliyowasikitisha. Wakuu wao akawamwagia masimango, akawatangishatangisha maporini kusiko na njia zo zote. Lakini mkiwa alimkingia yale mateso, asifikiwe nayo, akaviweka vizazi vyake kuwa vingi kama kondoo. Wanyokao mioyo walipoviona wakavifurahia kwamba: Wapotovu wote hufumbwa vinywa! Yuko nani aliye mwenye ujuzi? Na ayashike haya! Na autambue upole wake Bwana! E Mungu, moyo wangu umetulia na kushupaa, niimbe na kupiga shangwe! Ndio utukufu wangu. Amkeni, pango na zeze, niiamshe mionzi ya jua! Kwenye makundi ya watu wako nitakushukuru, Bwana nako kwenye wamizimu nitakuimbia. Kwani upole wako ni mkubwa, unatutokea toka mbinguni, nako mawinguni unafika welekevu wako. Utukuke, Mungu, juu mbinguni! Nazo nchi zote ziuone utukufu wako! Kusudi wao, uwapendao, wapate kuopoka, mkono wako wa kuume uwaokoe, ukutuitikia! Mungu alisema hapo Patakatifu pake: Nikiigawanya nchi ya Sikemu nitapiga vigelegele: ndipo, nitakapolipimanalo bonde la Sukoti. Gileadi ni yangu, Manase ni yangu Efuraimu ni kingio la kichwa changu, Yuda ni bakora yangu ya kifalme. Moabu ni bakuli langu la kunawia, Edomu ndiko, nitakakovitupia viatu vyangu, nchi ya Wafilisti nitaishangilia. Yuko nani atakayenipeleka mjini mwenye maboma? Yuko nani atakayeniongoza mpaka Edomu? Si wewe Mungu uliyenitupa, ukakataa kwenda vitani na vikosi vyetu? Tujie, utusaidie, tumshinde atusongaye! Kwani watu hawawezi kutuokoa. Kwa nguvu yake Mungu na tufanye nasi yenye nguvu! yeye ndiye atakayewakanyaga watusongao. Mungu, nikushangiliaye, usinyamaze! Kwani waisokucha na wadanganyifu wamenifumbulia vinywa, wakasema na mimi kwa ndimi zilizo zenye uwongo. Maneno yenye machukivu yakanizunguka; lakini wakinigombeza hivyo, hakuna sababu yo yote. Kwa hivyo, ninavyowapenda, wananipingia, nami naliwaombea wao hao. Kweli kwa mema, niliyowafanyizia, wananirudishia mabaya, kwa upendo wangu wananirudishia uchukivu. Weka mtu asiyekucha, amwangalie aliye hivyo! Satani mwenyewe amsimamie kuumeni kwake! Kwenye hukumu sharti atokezwe kuwa mwenye kushindwa, nako kuomba kwake sharti kuwaziwe kuwa kukosa! Siku zake na zifupizwe kuwa chache! Mtu mwingine na autwae ukaguzi wake! Watoto wake na waachwe peke yao! Naye mkewe na awe mjane! Wanawe na waje kutangatanga na kuombaomba kwa kufukuzwa kwenye mahame yao, wakijitafutia vyakula! Mkopeshaji na ajitwalie yote yaliyo yake, tena wageni na wapokonye aliyoyapata na kuyasumbukia! Pasiwepo anayemwendea kwa upole, wala pasiwepo anayewahurumia watoto wake walioachwa peke yao! Watoto, atakaowaacha, sharti waje kung'olewa, katika kizazi cha pili sharti jina lao litoweke! Manza, baba zake walizozikora na zikumbukwe kwake Bwana! Makosa ya mama yake yasifutwe, yawepo machoni pake Bwana siku zote! Aung'oe ukumbusho wao katika nchi! Kwa sababu hakukumbuka kufanya yenye upole, akawakimbiza kwake wanyonge na wakiwa nao waliopondeka mioyo, awaue kabisa. Apizo, alilolipenda, na limjie mwenyewe! Kwa kuwa hakupendezwa na mbaraka, na imkalie mbali naye! Akajivika apizo, kama ni kanzu yake, likamwingia moyoni, kama ni maji, au kama ni kiini kilichomo katika mifupa yake. Na limwie kama vazi la kujifunika, au kama mshipi, anaojifunga siku zote! Hayo Bwana awalipishe wao wanipingiao, nao wanaoisingizia roho yangu kuwa yenye mabaya! Nawe Mungu, Bwana wangu, nifanyizie yalipasayo Jina lako! Kwa kuwa upole wako ni mwema, nipoe! Kwani mimi ni mnyonge hata mkiwa, nao moyo wangu humu kifuani mwangu umeumia. Ninajiendea kama kivuli kinachojivuta, ninafukuzwa kama funutu. Magoti yangu yamelegea kwa kufunga mifungo, nyama za mwili wangu zimekonda, hazina mafuta. Kwa hiyo mimi nimekuwa kwao mtu wa kumsimanga, wanaponiona huvitingisha vichwa vyao. Nisaidie Bwana, Mungu wangu! Niokoe kwa upole wako! Ndipo, watakapoujua mkono wako, ya kuwa ndio, tena watajua, ya kuwa umeyafanya, wewe Bwana. Wao na waapize! Nawe na ubariki! Wakiinuka na wapatwe na soni, mtumishi wako afurahi! Sharti wavikwe mabezo wao wanipingiao, soni zao ziwafunika kama nguo! Na nimshukuru Bwana sanasana kwa kinywa changu! Kwenye watu wengi na nimshangilie! Kwani aliye mkiwa humsimamia kuumeni kwake, amwokoe mikononi mwao waliompatiliza. *Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti kuumeni kwangu, mpaka niwaweke adui zako chini miguuni pako! Bakora yako ya kifalme yenye nguvu Bwana ataituma toka Sioni: Katikati ya adui zako tawala wewe! Walio ukoo wako watakutokea kwa kupenda wenyewe siku iyo hiyo, utakapokwenda vitani; hapo watakuwa wamevaa mapambo yapasayo Patakatifu. Wana wako watazaliwa, kama umande unavyozaliwa asubuhi mapema. Bwana aliapa, naye hatajuta: Wewe u mtambikaji wa kale na kale, kama Melkisedeki alivyokuwa.* Bwana alioko kuumeni kwako atawaponda wafalme; itakuwa siku hiyo, makali yake yatakapotokea. Atakapohukumu kwenye wamizimu, ndipo, mizoga yao itakapojaa, akiwaponda vichwa mahali palipo papana. Atakunywa maji ya mtoni huko njiani, kwa hiyo atakiinua kichwa chake. Haleluya! *Namshukuru Bwana kwa moyo wote kwenye mkutano wao wanyokao mioyo nako kwao wateule. Matendo yake Bwana ni makubwa, yanachunguzika kwao wote wapendezwao nayo. Kazi zenye urembo na utukufu ndizo zake, wongofu wake husimama kale na kale. Alifanya ukumbusho wa vioja vyake, yeye Bwana aliye mwenye utu na mwenye huruma. Huwapa vilaji wao wamwogopao, Agano lake hulikumbuka kale na kale. Matendo yake yenye nguvu huyatangazia walio ukoo wake, awape nao urithi uliokuwa wao wamizimu. Matendo ya mikono yake ni yenye welekevu na yenye wongofu, maagizo yake yote yanategemeka, maana yalishikizwa kuwa ya kale na kale, hufanyizwa kwa welekevu na kwa unyofu. Walio ukoo wake aliwapatia ukombozi, akaagiza, Agano lake liwepo kale na kale. Jina lake ni takatifu, linaogopesha. Kumcha Bwana ndio mwanzo wa werevu wa kweli; huu ndio utambuzi mwema kwao wote wafanyao hivyo. Matukuzo yake husimama kale na kale.* Haleluya! Mwenye shangwe ni mtu amwogopaye Bwana, apendezwaye sana na maagizo yake. Wao wa uzao wake watakuwa wenye nguvu sana katika nchi hii, maana wanyokao mioyo vizazi vyao hubarikiwa. Malimbiko ya mali yamo nyumbani mwake, nao wongofu wake husimama kale na kale. Penye giza mwanga huwazukia wanyokao mioyo, ndio wenye utu na huruma nao wenye wongofu. Mtu mwenye huruma kwa kukopesha ataona mema, yeye atayatengeneza mashauri yake, yashinde kwenye hukumu. Kwani hatatikisika kale na kale, mwongofu ni mtu atakayekumbukwa kale na kale. Masingizio mabaya hayaogopi, moyo wake umeshupaa, maana humwegemea Bwana. Kwa kuwa na msingi wa moyo wake haogopi kamwe, mpaka atakapoona, wanavyofanyiziwa wao wamsongao. Alizimwaga mali zake, akawagawia wao waliozikosa; huu wongofu wake hukaa kale na kale, baragumu lake huwa limeelekezwa juu kwa kuwa lenye utukufu. Asiyemcha Mungu anaviona na kukasirika, hukereza meno, mwisho hupotea, tamaa zao wasiomcha Mungu huangamia. Haleluya! Ninyi watumishi wake Bwana, shangilieni! lishangilieni Jina lake Bwana! Jina lake Bwana na likuzwe kuanzia sasa hata kale na kale! Toka maawioni kwa jua mpaka machweoni kwake Jina lake Bwana na lishangiliwe! Bwana anatukuka kuwapita wamizimu wote, utukufu wake unaupita nao wake mbingu. Afananaye na Bwana Mungu wetu yuko nani? Naye alijipatia kao huko juu. Anajinyenyekeza, ayatazame yaliyoko mbinguni nayo yaliyoko nchini. Humsimamisha akorofikaye na kumwinua uvumbini, naye mkiwa humkweza na kumtoa kwenye taka, amkalishe pamoja nao walio wakuu, kweli pamoja nao wakuu wao wlaio ukoo wake. Naye mwanamke akosaye watoto humweka nyumbani kuwa mama ya watoto wenye furaha. Waisiraeli walipotoka kule Misri, wa mlango wa Yakobo walipotoka kwao wasemao msemo mgeni, Ndipo, Yuda alipopata kuwa mwenye Patakatifu pao, naye Isiraeli mwenye ufalme wao. Bahari ilipoviona, ilikimbia, mto wa Yordani nao ukarudi nyuma. Milima ikarukaruka kama kondoo waume, navyo vilima vidogo kama wana wa kondoo. Wewe, bahari, ulionaje ulipokimbia? Wewe Yordani nawe, uliporudi nyuma? Nanyi milima, mliporukaruka kama kondoo waume? Nanyi vilima vidogo, mliporukaruka kama wana wa kondoo? Tetemeka, wewe nchi, Bwana akitokea, Mungu wake Yakobo akitokea mwenyewe! Anaugeuza mwamba kuwa ziwa la maji, nayo mawe magumu kuwa mboji za maji. Sisi sio, Bwana, sisi sio tupaswao na kutukuzwa, ila Jina lako sharti ulipatie utukufu kwa ajili ya upole wako na kwa ajili ya welekevu wako. Mbona wamizimu wanasema: Mungu wao yuko wapi? Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, yote yampendezayo huyafanya. Vinyago vyao ni fedha na dhahabu, mikono ya watu ndiyo iliyovifanya: vinywa vinavyo, lakini havisemi, macho vinayo, lakini havioni, masikio vinayo, lakini havisikii, pua vinazo, lakini havinusi, mikono vinayo, lakini havipapasi, miguu vinayo, lakini haviendi, wala havisemi kwa koo zao. Kama hivyo vilivyo, ndivyo, watakavyokuwa nao waliovifanya, nao wote pia waviegemeao. Wewe Isiraeli, mwegemee Bwana! Yeye ni msaada wao na ngao yao. Ninyi mlio wa mlango wa Haroni, mwegemeeni Bwana! Yeye ni msaada wao na ngao yao. Ninyi mmwogopao Bwana, mwegemmeni Bwana! Yeye ni msaada wao na ngao yao. Bwana hutukumbuka, atubariki. Ataubariki mlango wao wa Waisiraeli, ataubariki nao mlango wake Haroni. Atawabariki wao wamwogopao Bwana, walio wadogo pamoja nao walio wakubwa. Bwana ataendelea kuwafanyia hivyo ninyi nao wana wenu watakaokuwa. Ninyi ndio mliobarikiwa naye Bwana aliyezifanya mbingu hata nchi. Mbingu ni mbingu zake yeye Bwana, nchi aliwapa wana wa watu. Bwana hawamshangilii walio wafu, wala wote walioshukia huko kuliko kimya. Lakini sisi na tumkuze Bwana kuanzia sasa, hata kale na kale! Haleluya! Nampenda Bwana, kwa kuwa husikia, huisikia sauti yangu, nikimlalamikia. Kwa kuwa hunitegea nami sikio lake, kwa hiyo nitamwitia siku zangu zote. Matanzi ya kifo yalikuwa yameninasa, masongano ya kuzimu yakanipata, kwa kuona masikitiko nikasongeka. Nikalililia Jina la Bwana ya kwamba: Wewe Bwana, iopoe roho yangu! Bwana ni mwenye utu na mwenye wongofu, kwa kuwa Mungu wetu hutuonea uchungu. Walio kama wachanga Bwana huwalinda; nilipokuwa mnyonge, aliniokoa. Rudi, roho yangu, kwenye kituo chako! Kwani Bwana ndiye aliyekutendea mema. Maana umeiopoa roho yangu katika kufa, ukafuta machozi machoni pangu, ukaishika miguu yangu, isijikwae. Kwa kumtazamia Bwana nitaendelea vivyo hivyo katika nchi zao walio hai. Nilikuwa nimemtegemea, kwa hiyo na niseme! Lakini nimeteseka sana mimi nami. Hapo, niliposhikwa na woga, nilisema mimi: Watu wote walioko ni wenye uwongo. Nitawezaje kumrudishia Bwana mema yote, aliyonitendea? Nitakiinua kinyweo chenye wokovu, kisha nitalitambikia Jina lake Bwana. Nitamlipa Bwana, niliyomwapia, wote walio ukoo wake wavione na macho yao. Ni jambo kuu machoni pa Bwana, wamchao wakifa. Mimi nakuomba, Bwana, mimi mtumishi wako, mimi mtumishi wako ni mwana wa mjakazi wako, nawe umenifungulia mafungo yangu. Nitakutolea wewe vipaji vya tambiko vya kukushukuru, kisha nitalitambikia Jina lake Bwana. Nitamlipa Bwana, niliyomwapia, wote walio ukoo wake wavione na macho yao, katika nyua zake Nyumba ya Bwana, katikati mjini mwako, wewe Yerusalemu. Haleluya! Mshangilieni Bwana, ninyi wamizimu wote! ninyi makabila yote ya watu, msifuni! Kwani upole wake hutenda makuu kwetu sisi, nao welekevu wake Bwana ni wa kale na kale! Haleluya! Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema! Ya kuwa upole wake ni wa kale na kale! Waisiraeli na waseme: Upole wake ni wakale na kale! Walio wa mlango wa Haroni na waseme: Upole wake ni wa kale na kale! Wamwogopao Bwana na waseme: Upole wake ni wa kale na kale! Niliposongeka nalimwita Bwana, naye Bwana akaniitikia na kunipanulia. Bwana akiwa upande wangu, sitaogopa; maana aliye mtu atanifanyia nini? Bwana akiwa upande wangu na kunisaidia, ndipo, nitakapowafurahia wachukivu wangu. Kumkimbilia Bwana kunafaa kuliko kuegemea watu. Kumkimbilia Bwana kunafaa kuliko kuegemea wakuu. Wamizimu wote walikuwa wamenizunguka, vikawa kwa nguvu ya Jina la Bwana, nikiwaponda. Kweli walikuwa wamenizungukana kunizinga, vikawa kwa nguvu ya Jina la Bwana, nikiwaponda. Walikuwa wamenizunguka kama nyuki, wakazimia upesi kama moto wa miiba; vikawa kwa nguvu ya Bwana, nikiwaponda. Walizidi kunikumba, nianguke, lakini Bwana akanisaidia. *Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, maana alinijia, akawa mwokozi wangu. Shangwe za kuushangilia wokovu huu husikilika kwenye vituo vyao waongofu: Mkono wa kuume wa Bwana hufanya yenye nguvu! Mkono wa kuume wa Bwana umetukuka, mkono wa kuume wa Bwana hufanya yenye nguvu! Sitakufa, ila nitakuwapo, niyasimulie matendo ya Bwana. Kweli Bwana hunichapa, lakini hanitoi, nife. Nifungulieni malango ya kuingia kwake wongofu, niingie humo, nimshukuru Bwana! Hili ndilo lango la kuingia mwake Bwana; waongofu ndio watakaoliingia. Ninakushukuru, kwa kuwa uliniitikia, maana ulinijia, ukawa mwokozi wangu. Jiwe, walilolikataa waashi, limekuwa la pembeni. Hivyo vimefanywa na Bwana; nasi tukivitazama, ni vya kustaajabu. Hii ni siku, Bwana aliyoitengeneza; na tushangilie na kuifurahia!* E Bwana, tunakuomba: Tuokoe! E Bwana, tunakuomb: Tupe kushinda! Na atukuzwe ajaye kwa Jina la Bwana! Tuliomo Nyumbani mwake Bwana tunawabariki ninyi. Bwana ni Mungu atuangazaye. Jipambieni sikukuu na kushika makuti, mje kufika kwenye pembe za meza iliyo ya kutambikia! Mungu wangu ni wewe, ninakushukuru; Mungu wangu, ninakutukuza. Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema! ya kuwa upole wake ni wa kale na kale! Wenye shangwe ndio wao wanaofuata njia zisizokosesha, wanaoendelea kuyafuata Maonyo yake Bwana. Wenye shangwe ndio wao wanaoyashika mashuhuda yake, wanaomtafuta yeye kwa mioyo yote. Hawafanyi mapotovu hata kidogo, ila njia zake ndizo, wanazoendelea kuzishika. Amri zako ulizitoa wewe mwenyewe, watu wazishike kabisa na kuzifuata. Ninataka sana, njia zangu zishupazwe, niyashike maongozi yako. Kwa kuyatazama maagizo yako yote sitatwezeka. Na nikushukuru kwa moyo unyokao, nikijifundisha wongofu wako wa kuamua. Na niyashike maongozi yako na kuyafuata, nawe usiniache, niwe peke yangu. Kijana ataiangaliaje njia yake, iwe imetakata? Itakuwa hapo, atakapolishika Neno lako na kulifuata. Nimekutafuta kweli kwa moyo Wangu wote, usiniache, nikapotea na kutoka kwenye maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka Neno lako, nisije kukukosea. Utukuzwe, wewe Bwana! Nifundishe maongozi yako! Kwa midomo yangu nimeyasimulia maamuzi yote ya kinywa chako nikaifurahia njia ya mambo, uliyoyashuhudia wewe, kama watu wanavyofurahiwa na mali zo zote. Amri zako na niziwaze moyoni na kuzitazama njia zako. Na nijichangamshe kwa maongozi yako, nisilisahau Neno lako! Mtendee mema mtumishi wako, nipate uzima tena! Na nilishike Neno lako na kulifuata! Yafumbue macho yangu, nipate kuona, niyaone mataajabu yatokeayo kwenye Maonyo yako. Mimi ni mgeni katika nchi, usinifiche maagizo yako! Roho yangu imepondeka kwa kuyatunukia hayo maamuzi yako mchana kutwa. Uliwakaripia wenye majivuno, wakawa wameapizwa, wakapotea kwa kuyaacha maagizo yako. Ondoa kwangu matwezo na mabezo! Kwani nayashika mashuhuda yako. Wako nao wakuu wanaopiga mashauri ya kuniteta, lakini mtumishi wako anayoyawaza moyoni, ndiyo maongozi yako. Mashuhuda yako hunichangamsha, ndiyo yanayoniongoza. Ambayo roho yangu imegandamana nayo, ndiyo mavumbi; kwa hivi nirudishe uzimani, kama ulivyosema! Nilipokusimulia, njia zangu zilivyo, uliniitikia; unifundishe maongozi yako, niyajue! Unitambulishe njia ya amri zako, niyawaze mataajabu yako! Roho yangu imeyeyuka kwa ukiwa; niinue, kama ulivyosema! Njia ya uwongo ipitishe mbali, nisiione! Kwa huruma zako nipe kuyashika Maonyo yako! Njia yenye kweli ndiyo, niliyoichagua, maamuzi yako nimeyaweka machoni pangu. Ambayo nimegandamana nayo, ndiyo mashuhuda yako; Bwana, usiniache, nikatwezwa! Nitapiga mbio, nifike njiani kwa maagizo yako, kwani moyo wangu umeupatia mahali papana. Nifunze, Bwana, niijue njia ya maongozi yako, niishike na kuifuata mpaka mwisho! Nitambulishe Maonyo yako, niyashike, niyaangalie na kuyafuata kwa moyo wote. Niendeshe katika mkondo wa maagizo yako! Kwani yanayonipendeza ndiyo hayo. Uelekeze moyo wangu, uyatazame mashuhuda yako, usiyatazame tena mapato ya faida. Yapitishe macho yangu, yasitazame mambo ya bure, ila yazitazame njia zako zinipazo uzima! Mpatie mtumishi wako uliyomwambia! Naye akuogope! Pitisha kwangu mambo yanitiayo soni! Kwani ninayaogopa, maana maamuzi yako ndiyo yaliyo mema. Tazama, jinsi ninavyozitunukia amri zako! Nawe kwa wongofu wako nipe uzima! Magawio ya upole wako, Bwana, na yanijie! Uniokoe, kama ulivyosema! Hivyo ndivyo, nitakavyomjibu anitukanaye, kwani egemeo langu ni Neno lako. Usiliondoe kabisa kinywani mwangu hilo Neno lililo kweli! Kwani maamuzi yako ndiyo, ninayoyangojea. Nami nitayaangalia Maonyo yako, niyafuate siku zote pasipo kukoma kale na kale. Nitajiendea palipo papana kwa kuzitafuta amri zako. Nayo mashuhuda yako nitayasimulia hata mbele ya wafalme pasipo kuona soni. Na nijichangamshe kwa maagizo yako, maana nimeyapenda. Hata mikono yangu nitaiinulia maagizo yako kwa kuyapenda, nayo maongozi yako nitayawaza moyoni. Likumbuke Neno lako, ulilomwambia mtumishi wako! Maana ulisema, nilingojee. Hili ndilo lililonituliza moyo katika mateso yangu, kwani Neno lako ndilo lililonirudisha uzimani. Wenye majivuno hunifyoza na kuzidi sanasana, lakini sikuondoka kwenye Maonyo yako. Ninapoyakumbuka maamuzi yako, Bwana, uliyoyaamua tangu kale, ndipo, ninapoutuliza moyo wangu. Makali yenye moto yalikuwa yamenishika kwa ajili yao wasiokucha, walioyaacha nayo Maonyo yako. Maongozi yako ndiyo, ninayoyaimbia namo nyumbani, nilimotua nilipokuwa mgeni. Jina lako, Bwana, nalikumbuka nao usiku, niyashike Maonyo yako, niyafuate. Hizo ndizo mali zangu, nilizozipata, kwa kuwa nimezishika amri zako. Bwana ni fungu langu! ndivyo, nilivyosema; kwa hiyo nayashika maneno yako na kuyafuata. Nikakulalamikia usoni pako kwa moyo wote, unihurumie, kama ulivyoniambia. Nilipozitazama njia zangu, nikairudisha miguu yangu, nikaielekeza, iyafuate mashuhuda yako. Sikujizuzua na mambo mengine mengine, ila nikapiga mbio. niyashike maagizo yako na kuyafuata. Matanzi yao wasiokucha yalikuwa yamenizunguka, lakini Maonyo yako sikuyasahau. Nikiamka usiku wa manane, ninakushukuru, kwa ajili ya wongofu wako wa kuamulia watu. Wenzangu mimi ndio wote wakuogopao wewe, wanaozishika amri zako na kuzifuata. Upole wako, Bwana, ndio ulioieneza nchi. Nifundishe maongozi yako, niyajue! Mtumishi wako umemfanyizia mema, kama ulivyosema, Bwana. Nifundishe utambuzi na ujuzi ulio mwema! Kwani maagizo yako nimeyategemea. Nilipokuwa sijanyenyekezwa bado, nilikuwa nimepotea lakini sasa nimelishika Neno lako, nilifuate. Wewe ndiwe mwema, hufanya mema; nifundishe maongozi yako, niyajue. Wenye majivuno wametunga uwongo wa kunisingizia, lakini mimi ninazishika amri zako kwa moyo wote. Mioyo yao imenenepa kama yenye unono, nami huyachangamkia Maonyo yako. Kule kunyenyekezwa kumenifaa kwa kunifundisha maongozi yako. Maonyo ya kinywa chako ni mema kwangu kuliko maelfu ya vipande vya dhahabu na vya fedha. Mikono yako iliniumba na kunitengeneza; nipe kuvitambua, nijifundishe maagizo yako! Wakuogopao hufurahi wakiniona mimi, kwani Neno lako ndilo, ninalolingojea. Nimeyajua maamuzi yako, Bwana, kuwa yenye wongofu, maana umeninyenyekeza kwa welekevu. Upole wako sharti uje, unitulize moyo, kama wewe ulivyomwambia mtumishi wako. Machungu yako, uliyonionea, na yaje, nipatekuwa mzima tena! Kwani Maonyo yako hunichangamsha. Wenye majivuno watapatwa na soni, kwani hunipotoa bure, lakini moyoni mwangu mimi ninaziwaza amri zako. Wakuogopao na waje kuwa upande wangu pamoja nao wale wayajuao mashuhuda yako. Moyo wangu sharti uwe pasipo kosa kwa nguvu ya maongozi yako, kusudi soni za kunipata zisinijie. Roho yangu imezimia kwa kuutunukia wokovu wako, lakini Neno lako ndilo, ninalolingojea. Nayo macho yangu yamepata kiwi kwa kulichungulia Neno lako kwa kwamba: Itakuwa lini, utakaponituliza moyo? Kwani nimekuwa kama kiriba kilichoanikwa katika moshi, lakini maongozi yako sikuyasahau. Siku za mtumishi wako zilizobaki ni ngapi tena? Utawahukumu lini wao wanikimbizao? Hawa wenye majivuno wamenichimbia mashimo, nao ndio wasioyafuata Maonyo yako. Maagizo yako yote ni ya welekevu; lakini wao hunikimbiza bure, kwa hiyo nisaidie! Ilikuwa imesalia kidogo, wangenitowesha huku nchini, lakini amri zako sikuziacha. Kwa upole wako nirudishe uzimani! Ndipo, nitakapoyashika na kuyafuata mashuhuda ya kinywa chako. Bwana, Neno lako ni la kale na kale, lilitiwa nguvu kule mbinguni. Welekevu wako hukalia vizazi na vizazi. Ulipozishikiza nchi, zikapata kusimama; zimesimama mpaka leo kwa hivyo, ulivyozitengeneza, kwani vinavyokutumikia ni vyote pia. Kama Maonyo yako yasingalinichangamsha, ningaliangamia kwa kuteseka. Kale na kale sitazisahau amri zako, kwani kwa nguvu zao umenirudisha uzimani. Niokoe mimi niliye wako kwa kuzitafuta amri zako. Wasiokucha huningojea, waniangamize; lakini mimi ninayatambua mashuhuda yako. Kila kitu niliuona mwisho wake, siku zake zilipotimia, lakini agizo lako halina mpaka. Maonyo yako nimeyapenda sanasana, ndiyo yaliyomo moyoni mwangu siku zote. Maagizo yako hunierevusha kuliko adui zangu, Kwani kale na kale ndiyo yaliyoko kwangu. Akili zangu huzipita zao wafunzi wangu wote, kwani mashuhuda yako ndiyo, niyawazayo moyoni. Kwa utambuzi ninawapita nao wazee, Kwani nimeziangalia amri zako. Miguu yangu nimeikataza kushika njia mbaya yo yote, nipate kulishika Neno lako na kulifuata. Kwenye maamuzi yako sikuepuka, kwani wewe mwenyewe ulinifundisha, niyajue. Maneno yako ni matamu peke yao katika ufizi wangu, kinywani mwangu ni matamu kweli kuliko asali. Katika amri zako ndipo, utambuzi wangu ulipotoka; kwa hiyo ninachukizwa na kila njia ya uwongo. Neno lako ni taa miguuni pangu, hunimulikia njiani pangu. Nimejiapia, tena nitayafanya, niushike wongofu wako wa kuamua, niufuate. Bwana, nimenyenyekezwa sanasana; nirudishe uzimani, kama ulivyosema! Vipaji, kinywa changu kinavyopenda kuvitoa, na vikupendeze, Bwana! Na unifundishe maamuzi yako, niyajue! Roho yangu nakupelekea mkononi mwangu siku zote, maana Maonyo yako sikuyasahau. Wamenitegea matanzi wao wasiokucha, lakini sikupotea na kuziacha hizo amri zako. Mashuhuda yako ndio fungu langu la kale na kale, kwani ndiyo yanayoufurahisha moyo wangu. Nimeuelekeza moyo wangu na kwako, uyafanye maongozi yako kale na kale mpaka mwisho. Walio wenye mioyo miwili nimechukizwa nao, lakini Maonyo yako nimeyapenda. Wewe ndiwe ficho langu na ngao yangu, nalo Neno lako ndilo, ninalolingojea. Ondokeni kwangu, ninyi mfanyao mabaya! Mimi ninataka kuyashika maagizo yake Mungu wangu. Nishikize, kama ulivyoniambia, nipate uzima tena! Usinitie soni! Maana nimekungojea. Unitie nguvu, nipate kuokoka! Nami na niyatazame maongozi yako siku zote! Unawatupa wote wapoteao na kuyaacha maongozi yako, kwani udanganyifu wao ni wa bure. Wote wasiokucha huku nchini unawazoa kama mitapo ya chuma, kwa hiyo nimeyapenda mashuhuda yako. Kwa kukuogopa sana nyama za mwili wangu zimeguiwa na kituko, nayo maamuzi yako ninayaogopa. Nimefanya yaliyo sawa yenye wongofu, usinitoe na kunitia mikononi mwao wanikorofishao. Jitoe kuwa kole ya mtumishi wako, aone mema, wenye majivuno wasinikorofishe! Macho yangu yamepata kiwi kwa kuuchungulia wokovu wako na kwa kulichungulia Neno lako lililo lenye wongofu. Mfanyizie mtumishi wako kwa upole wako! Nifundishe maongozi yako, niyajue! Mimi ni mtumishi wako, nipe utambuzi, nipate kuyajua mashuhuda yako! Siku zimetimia, Bwana afanye kitu, maana Maonyo yako wameyatengua. Kwa hiyo nimeyapenda hayo maagizo yako kuliko dhahabu, ijapo ziwe nzuri zaidi. Kwani ninaziwazia amri zako zote kuwa za wongofu, lakini njia yo yote ya uwongo nimechukizwa nayo. Mashuhuda yako ni ya kustaajabu; hii ndiyo sababu, roho yangu ikiyashika. Maneno yako yakifunuliwa huangaza, huwapa utambuzi nao waliopumbaa. Nimekifumbua kinywa changu, nikatweta kwa kuyatunukia maagizo yako. Geuka, unielekee mimi na kunihurumia, kama inavyowapasa wao walipendao Jina lako! Mwenendo wangu uutie nguvu, ulifuate Neno lako, upotovu uwao wote usije kunitawala! Katika makorofi ya watu na unikomboe! Nami na nizishike amri zako na kuzifuata! Mwangazie mtumishi wako uso wako, unifundishe maongozi yako, niyajue! Macho yangu yanatoka vijito vya maji kwa ajili yao wasioyashika Maonyo yako na kuyafuata. Wewe Bwana ndiwe mwongofu, nayo maamuzi yako kunyoka. Mambo yanayopasa, uyashuhudie wewe, umeyaagiza kuwa yenye wongofu na welekevu kabisa. Wivu wa kunija umenizimisha roho, kwani wameyasahau maneno yako wao wanisongao. Neno lako liko, limeng'azwa kabisa, kwa hiyo amelipenda mtumishi wako. Mimi ni mdogo, ninabezwa, lakini amri zako sikuzisahau. Wongofu wako ndio wongofu ulio wa kale na kale, nayo Maonyo yako ndiyo ya kweli. Masongano na mahangaiko yamenipata, lakini maagizo yako ndiyo yanayonichangamsha. Mashuhuda yako ni yenye wongofu kale na kale, nipe kuyatambua, nipate uzima tena! Nimeita kwa moyo wangu wote, niitikie, Bwana! Maongozi yako na niyashike! Nimekuita wewe, na uniokoe! Nami nitayashika mashuhuda yako na kuyafuata. Nimejidamka na mapema, nikulilie, Neno lako ndilo, ninalolingojea. Zamu za usiku zinapokuwa hazijapokeana, niko macho, nipate kuliwaza Neno lako moyoni mwangu. Isikie sauti yangu kwa upoke wako! Bwana, kwa hivyo, maamuzi yako yalivyo, nirudishe uzimani! Wakimbiliao mapotovu wamenikaribia, ndio watu walioyaacha mbali Maonyo yako. Wewe, Bwana, uko karibu, nayo maagizo yako yote ndiyo ya kweli. Tangu kale ninayajua mashuhuda yako, nayo yalinifundisha, ya kuwa uliyawekea msingi, yawepo kale na kale. Utazame ukiwa wangu, uniopoe! Kwani Maonyo yako sikuyasahau. Nigombee kondo yangu, unikomboe! Nirudishe uzimani, kama ulivyoniambia! Wokovu unawakalia mbali wao wasiokucha, kwani hawakuyatafuta maongozi yako! Huruma zako, Bwana, ulizotupatia, huwa nyingi, kwa hivyo, maamuzi yako yalivyo, nirudishe uzimani! Wanaonikimbiza nao wanaonisonga ndio wengi, lakini sikuondoka na kuyaacha mashuhuda yako. Nikiwatazama waliorudi nyuma kwa udanganyifu najiliwana kutapika, kwa kuwa hawakulishika Neno lako na kulifuata. Tazama, jinsi ninavyozipenda amri zako! Bwana, kwa upole wako nirudishe uzimani! Neno lako lote zima ni la kweli, wongofu wako wa kuamua yo yote ni wa kale na kale. Wao walionikimbiza bure ndio wakuu, lakini moyo wangu unaloliogopa sana, ni Neno lako. Mimi ninayafurahia, uliyoyasema, kama mtu atokaye vitani mwenye mateka mengi. Uwongo nimeuchukia, hunitapisha; Maonyo yako ndiyo, ninayoyapenda. Ninakushangilia kila siku mara saba zote kwa ajili ya wongofu wako wa kuamulia watu. Wayapendao Maonyo yako hupata utengemano mwingi, hawaoni lo lote litakalowakwaza. Bwana, wokovu wako nimeutazamia, nayo maagizo yako nimeyafanya. Roho yangu imeyashika na kuyafuata mashuhuda yako, maana nimeyapenda sanasana. Nimezishika amri zako na kuzifuata, nayo mashuhuda yako, kwani njia zangu zote ziko machoni pako. Malalamiko yangu na yakufikie karibu usoni pako, Bwana! Kama ulivyosema, nipe utambuzi! Maombo yangu na yakujie usoni pako! Kama ulivyoniambia, uniponye! Shangwe na zifurike midomoni mwangu, kwa kuwa ulinifundisha maongozi yako! Ulimi wangu na uliitikie Neno lako! Kwani maagizo yako yote ni yenye wongofu. Mkono wako na uje kunisaidia mimi! Kwani amri zako ndizo, nilizozichagua. Wokovu wako, Bwana, nimeutunukia, nayo Maonyo yako ndiyo yanayonichangamsha. Roho yangu na ipate uzima tena, ikushangilie! Nayo maamuzi yako na yanisaidie! Nikipotelewa na njia kama kondoo aliyepotea, mtafute mtumishi wako! Kwani sikuyasahau maagizo yako. Nilipomwita Bwana katika masongano yangu, akaniitikia. Bwana, iponye roho yangu, nisishindwe nao wanaonijia kwa midomo yenye uwongo na kwa ndimi za kudanganya! Ninyi ndimi zenye udanganyifu, atawapa nini? Kisha yako mambo gani tena, atakayoendelea kuwapatia ninyi? Maana zinakuwa kama mishale ya mpiga vita iliyotiwa ukali, au kama makaa ya mshuluti yaliyo yenye moto mwingi. Ukiwa wangu ni kukaa ugenini huku Meseki na kutua katika mahema yao watu wa Kedari. Kwa kukaa huku siku nyingi roho yangu inahangaika, maana watu wa huku huuchukia nao utengemano. Mwenye utengemano ndio mimi, lakini ninaposema nao, wao hutafuta magomvi. Ninayainua macho yangu na kuyaelekeza milimani, kwani ndiko, utakakotoka msaada wangu. Msaada wangu hutoka kwake Bwana, ndiye aliyeziumba mbingu na nchi. Hatautoa mguu wako, uje kujikwaa, maana halali usingizi akulindaye. Tazameni! Halali usingizi, wala hasinzii yeye aliye mlinzi wake Isiraeli. Bwana ndiye akulindaye, Bwana ni kivuli chako kuumeni kwako, mchana jua lisikuumize, wala mwezi usiku. Bwana atakukingia mabaya yote, atailinda roho yako. Bwana na akulinde kutoka kwako na kuingia kwako kuanzia sasa hata kale na kale! *Niliwafurahia walioniambia: Twende Nyumbani kwa Bwana! Hivyo miguu yetu iko ikisimama malangoni kwako, Yerusalemu. Yerusalemu umejengwa tena kama mji ulioungamanishwa vema. Ndiko, mashina ya watu yanakopanda, yaliyo mashina ya Bwana; ndiko, wanakowashuhudia Waisiraeli, walishukuru Jina la Bwana. Kwani viti vya uamuzi vilipowekwa, ndipo pale, ni viti vya kifalme vya mlango wa Dawidi. Uombeeni Yerusalemu utengemano, watengemane nao waupendao! Sharti uwe utengemano ndani ya boma lako, nao utulivu katika majumba yako yaliyo mazuri mno. Kwa ajili yao walio ndugu zangu na rafiki zangu na niseme tena na kuomba: Utengemano na uwe kwako! Kwa ajili ya Nyumba ya Bwana Mungu wetu na nikutafutie mema.* Nimeyainua macho yangu na kuyaelekeza kwako, ukaaye mbinguni. Kama macho ya watumishi yanavyoitazama mikono ya bwana zao, au kama macho ya mjakazi yanavyoitazama mikono ya bibi yake, hivyo macho yetu humtazama Bwana Mungu wetu, hata atuhurumie. Tuhurumie, Bwana! Tuhurumie! Kwani tumeshiba sana mabezo. Roho zetu zimeshiba sana masimango yao wanaokula vya urembo, nayo mabezo yao wenye majivuno. Kama Bwana asingalikuwa nasi, Waisiraeli na waseme hivyo: Kama Bwana asingalikuwa nasi, watu walipotuinukia, wangalitumeza, tukingali wazima bado; ilikuwa hapo, moto wa makali yao ulipotuunguza. Maji mengi yangalitudidimiza hapo, mito ilipopita juu yetu, kwani hapo mafuriko ya maji yaliyopita juu yetu yangalitutosa kweli. Bwana na asifiwe! Kwani hakututoa, tunyafuliwe na meno yao! Roho zetu zimepona, kama ndege anavyopona tanzini, kamba za tanzi zikikatika; ndivyo, sisi tulivyopona nasi. Msaada wetu uko katika Jina la Bwana, ndiye aliyeziumba mbingu na nchi. Wamwegemeao Bwana hufanana nao mlima wa Sioni, hautikisiki, unakaa kale na kale. Kama milima inavyouzunguka mji wa Yerusalemu, ndivyo, Bwana anavyowazunguka walio ukoo wake kuanzia sasa hata kale na kale. Kwani bakora yao wasiomcha Mungu haitashika uflame wa kulitawala fungu lao walio waongofu, kusudi waongofu wasiipeleke mikono yao kushika yenye mapotovu. Bwana, walio wema wafanyizie mema, nao wanyokao mioyo! Lakini wao wazigeuzao njia zao kuwa za kuptokapotoka Bwana an awaache, wajiendee pamoja nao wafanyao maovu! Utengemano na uwakalie wao Waisiraeli! *Bwana atakapowakomboa Wasioni waliotekwa akiwarudisha kwao, ndipo, tutakapokuwa kama watu wenye kuota ndoto: vinywa vyetu vitajaa macheko, nazo ndimi zetu zitapiga vigelegele. Ndipo, nao wamizimu watakaposema: Bwana amewafanyizia makuu! Kweli Bwana ametufanyizia mambo makuu, kwa hiyo twaona furaha. Bwana, wakomboe wenzetu waliotekwa ukiwarudisha kwetu, tuwe kama mito ya mchanga iliyojazwa maji na mvua ya vuli! Waliomiaga mbegu na kulia machozi ndio watakaovuna na kupiga vigelegele. Kweli waliokwenda njia zao na kulia machozi walipopeleka mbegu za kumiaga ndio watakaokuja na kupiga vigelegele wakichukua vicha, walivyovivuna.* Bwana asipoijenga nyumba, waijengao hujisumbua bure; Bwana asipoulinda mji, walinzi huwa macho bure. Ni bure mkijidamka mapema, tena mkichwelewa kazini, mkala chakula wenye machungu yasiyokoma mioyoni; kwani wamchao huwapa, wakiwa wamelala usingizi. Tazameni: Watoto ndio tunzo, Bwana ampatialo mtu, nao uzao wa tumbo ni kipaji chake. Kama mishale ilivyo katika mkono wa mpiga vita. ndivyo, wana wa kiume walivyo, wakiwa wenye nguvu za ujana. Mwenye shangwe ni mpiga vita aliyelijaza podo lake hao, hawa hawatatwezeka wakisemeana nao adui zao malangoni. Mwenye shangwe ni kila amwogopaye Bwana, azishikaye njia zake! Kwani utajilisha yayo hayo, mikono yako iliyoyasumbukia, kwa kuyapata hayo mema yako nawe u mwenye shangwe. Mke wako wa nyumbani mwako atafanana na mzabibu uzaao vizuri: watoto wako wataizunguka meza yako kama makuti ya mchikichi. Kwani ndivyo, mtu anavyobarikiwa akimwogopa Bwana. Bwana na akubariki toka Sioni, uyatazame mema ya Yerusalemu! Na uyaone na kuyafurahia siku zako zote za kuwapo, na uone nao watoto wa wanao! Utengemano na uwakalie Waisiraeli! Wamenisonga mara nyingi tangu ujana wangu; ndivyo, watakavyosema wao Waisiraeli. Wamenisonga mara nyingi tangu ujana wangu, lakini hawakupata kunishinda. Walimaji walilima mgongoni kwangu, wakatengeneza kuko huko matuta mazima. Lakini Bwana ni mwongofu, amezikata kamba zao wasiomcha. Sharti watwezwe na kurudishwa nyuma wote wachukizwao na Sioni! Sharti wawe kama majani yaliyoko kipaani juu ya nyumba! Miche yao hunyauka ikiwa haijachanua bado. Hapo mvunaji hawezi kukijaza kiganja chake tu, wala mfunga miganda hapajazi penye kifua chake. Wapitao wasiseme: Bwana na awabariki! Lakini ninyi tunawabariki katika Jina la Bwana. *Humu, nilimo vilindini, ninakulilia, Bwana. Ninakuomba, Bwana, uisikilize sauti yangu! Masikio yako na yaziangalie sauti za malalamiko yangu! Bwana, kama unazishika manza, watu walizozikora, yuko nani atakayesimama mbele yako wewe? Lakini kwako liko ondoleo la makosa, kusudi watu wakuogope. Ninamngojea Bwana, nayo roho yangu inamngojea, nalo Neno lake ndilo, ninalolitazamia. Roho yangu inamngoja Bwana, inashinda walinzi wa usiku, ndio walinzi wa usiku wanaongoja, kuche. Waisiraeli na wamngoje Bwana! Kwani kwake Bwana kuna upole, nao ukombozi uko kwake wa kukomboa wengi. Yeye atawakomboa Waisiraeli katika manza, walizozikora zote.* Bwana, moyo wangu haujikuzi, wala macho yangu hayatazami juu, wala sifuatii makuu na mataajabu yanishindayo nguvu, lakini nimeituliza roho yangu, nikainyamazisha. Kama mtoto anavyotulia kifuani kwa mama yake akiisha kuzoezwa, asinyonye tena, ndivyo, roho yangu inavyotulia kifuani mwangu, ikiwa kama mtoto aliyezoezwa hivyo. Waisiraeli na wamngoje bwana kuanzia sasa hata kale na kale! Bwana, mkumbukie Dawidi masumbuko yake yote! Yeye alimwapia Bwana, kisha akamwagia naye yule Mwenye nguvu aliye Mungu wa Yakobo: Sitaingia nyumbani mwangu, nilimotua, wala sitapanda kitandani pangu pa kulalia, nitayazuia macho yangu, yasipate uzingizi, nitaziangalia nazo kope zangu, zisisinzie, mpaka nitakapompatia Bwana mahali pa kuwapo, pawe makao yake Mwenye nguvu aliye Mungu wa Yakobo. Ndivyo, tulivyovisikia katika nchi ya Efurata, ndivyo, tulivyoviona mashambani kwenye misitu. Na tuingie hapo, makao yake yalipo! Na tumwangukie hapo, anapowekea miguu yake! Inuka, Bwana, uingie penya kituo chako, wewe na Sanduku la Agano lenye nguvu zako, watambikaji wako wajivike wongofu, wakuchao washangilie! Kwa ajili ya mtumishi wako Dawidi usiurudishe nyuma uso wake yeye, uliyempaka mafuta. Bwana alimwapia Dawidi kiapo cha kweli, naye hatakiacha akirudi nyuma: Walio uzao wa mwili wako nitawaketisha katika kiti chako cha kifalme, Kama wanao watalishika Agano langu, walifanye, kama watayashika hayo mashuhuda yangu, nitakayowafundisha, wana wao wataketi kale na kale katika kiti chako cha kifalme. Kwani Bwana aliuchagua mji wa Sioni, akaupenda, uwe Kao lake: Hapo ndipo, kitakapokuwa kituo changu cha kale na kale, hapo ndipo, nitakapokaa, kwani nimepapenda. Vilaji vyake nitavibariki, nao maskini wake nitawashibisha mikate. Watambikaji wake nitawavika wokovu, nao wanichao watapiga vigelegele. Hapo ndipo, nitakapolivumisha baragumu lake Dawidi, limpatie nguvu, naye, niliyempaka mafuta, nitamtengenezea taa. Walio adui zake nitawavika soni, lakini kichwani pake kitametameta kilemba, nilichomfunga. Utazameni wema na utamu ulioko huko, ndugu wanakokaa pamoja na kupatana Ni kama yale mafuta mazuri ya kichwani pake Haroni, yakishuka na kuziiingia ndevu zake zilizokuwa ndefu, zikafika mpaka kwenye pindo la kanzu yake. Au ni kama umande ulioko Hermoni, nako kwenye milima ya Sioni unakufika. Kwani Bwana alikoagizia mbaraka, ndiko huko, kuwa kwenye uzima kale na kale. Mtukuzeni Bwana, nyote mlio watumishi wa Bwana, msimamao na usiku Nyumbani mwake Bwana! Iinueni mikono yenu hapo Patakatifu! Mtukuzeni Bwana! Bwana akubariki toka Sioni, yeye aliyeziumba mbingu na nchi! Haleluya! Lishangilieni Jina lake Bwana! Mlio watumishi wake Bwana, shangilieni! Nanyi msimamao Nyumbani mwake Bwana, nanyi mlioko nyuani penye Nyumba ya Mungu wetu, mshangilieni Bwana! Kwani Bwana ni mwema. Liimbieni Jina lake na kupiga mazeze! Kwani ni zuri. Kwani Bwana alimchagua Yakobo, awe wake, yeye Isiraeli awe mali zake. Kwani mimi ninajua, ya kuwa Bwana ni mkuu, ya kuwa Bwana wetu anaipita miungu yote kwa huo ukuu. Yote, apendezwayo nayo, Bwana huyafanya, ikiwa mbinguni au nchini, ikiwa baharini au kilindini pawapo pote. Yeye ndiye anayepandisha mawingu akiyatoa mapeoni kwa nchi, yeye ndiye anayefanya umeme na mvua pamoja, yeye ndiye anayeutoa nao upepo malimbikioni kwake. Yeye ndiye aliyewapiga kule Misri wazaliwa wa kwanza akianzia kwa watu, akimalizia kwao nyama. Yeye ndiye aliyetuma vielekezo na vioja, vikutokee kwako, wewe Misri, vimshinde Farao na watumishi wake wote. Yeye ndiye aliyepiga wamizimu wengi, akaua nao wafalme wenye nguvu, kama Sihoni, mfalme wa Waamori, na Ogi, mfalme wa Basani, hata nchi zote za Kanaani pamoja na wafalme wao. Akazitoa nchi zao, zitwaliwe, zitwaliwe nao walio ukoo wake wa Isiraeli, ziwe fungu lao. Bwana Jina lako ni la kale na kale, Bwana, ukumbuko wako ni wa vizazi na vizazi. Kwani Bwana atawaamulia walio ukoo wake kwa kuwaonea uchungu walio watumishi wake. Vinyago vya wamizimu ni fedha na dhahabu, mikono ya watu ndiyo iliyovifanya: vinywa vinavyo, lakini havisemi, macho vinayo, lakini havioni, masikio vinayo, lakini havisikii; wala pumzi hazimo vinywani mwao. Kama hivyo vilivyo, ndivyo, watakavyokuwa nao waliovifanya; nao wote pia waviegemeao. Mlio wa mlango wa Isiraeli, mtukuzeni Bwana! Mlio wa mlango wa Haroni, mtukuzeni Bwana! Mlio wa mlango wa Lawi, mtukuzeni Bwana! Mmwogopao Bwana, mtukuzeni Bwana! Bwana na atukuzwe mle Sioni, yeye akaaye Yerusalemu! Haleluya! Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema, ya kuwa upole wake ni wa kale na kale! Mshukuruni Mungu, aipitaye miungu, ya kuwa upole wake ni wa kale na kale! Mshukuruni Bwana wa mabwana, ya kuwa upole wake ni wa kale na kale! Ni yeye peke yake afanyaye mataajabu makuu, kwani upole wake ni wa kale na kale. Ndiye aliyezifanya mbingu kwa utambuzi wake, kwani upole wake ni wa kale na kale. Ndiye aliyeitandika nchi juu ya maji, kwani upole wake ni wa kale na kale. Ndiye aliyeifanya mianga mikubwa, kwani upole wake ni wa kale na kale. Jua alilipa kutawala mchana, kwani upole wake ni wa kale na kale. Mwezi pamoja na nyota alizipa kutawala usiku, kwani upole wake ni wa kale na kale. Ndiye aliyewapiga wazaliwa wa kwanza kule Misri, kwani upole wake ni wa kale na kale. Akawatoa Waisiraeli katika nchi yao, kwani upole wake ni wa kale na kale. Kwa nguvu za viganja vyake, alipoikunjua mikono yake, kwani upole wake ni wa kale na kale. Ndiye aliyeitenga Bahari Nyekundu, ikasimama pande mbili, kwani upole wake ni wa kale na kale. Akawapitisha Waisiraeli hapo katikati, kwani upole wake ni wa kale na kale. Ndiye aliyemtosa Farao na vikosi vyake katika Bahari Nyekundu, kwani upole wake ni wa kale na kale. Ndiye aliyewaongoza nyikani walio ukoo wake, kwani upole wake ni wa kale na kale. Ndiye aliyepiga wafalme wakuu, kwani upole wake ni wa kale na kale. Akawaua wafalme wenye nguvu, kwani upole wake ni wa kale na kale. Kama Sihoni, mfalme wa Waamori, kwani upole wake ni wa kale na kale. Na Ogi, mfalme wa Basani, kwani upole wake ni wa kale na kale. Akazitoa nchi zao, zitwaliwe, kwani upole wake ni wa kale na kale. Zitwaliwe na Waisiraeli walio watumishi wake, ziwe fungu lao, kwani upole wake ni wa kale na kale. Ndiye aliyetukumbuka, tulipokuwa tumenyenyekezwa, kwani upole wake ni wa kale na kale. Akatuponya na kutuokoa kwao watusongao, kwani upole wake ni wa kale na kale. Ndiye anayewapa vilaji wote walio wenye miili, kwani upole wake ni wa kale na kale. Mshukuruni Mungu aliye wa mbingu! Kwani upole wake ni wa kale na kale. Kwenye mito ya Babeli twalikaa na kulia tulipoikumbuka Sioni, katika mifuu iliyoko kule twaliyaangika mazeze yetu. Kwani kule waliotuteka walitushurutisha kuimba nyimbo, wao waliotuumiza walitaka, tuwachezee, wakasema: Tuimbieni wimbo wa Sioni! Lakini tungaliwezaje kuimba wimbo wa Bwana katika nchi ya ugeni? Kama ningekusahau, Yerusalemu, nao mkono wangu wa kuume na usahauliwe! Ulimi wangu sharti ugandamane na ufizi wangu, nisipokukumbuka, nisipoukweza Yerusalemu kuwa furaha yangu kuu kuliko nyingine zote. Bwana, wana wa Edomu na uwakumbukie, walivyoufanyizia Yerusalemu siku ile, waliposema: Bomoeni! Bomoeni mpaka kwenye misingi yake! Wewe binti Babeli, utakuwa mahame tu. Mwenye shangwe ndiye atakayekulipisha hayo matendo yako, uliyotutendea sisi. Mwenye shangwe ndiye atakayewakamata watoto wako wachanga na kuwaponda mwambani. Kwa moyo wangu wote nitakushukuru, nitakuimbia na kupiga zeze mbele ya miungu. Penya Nyumba yako takatifu nitakutambikia, nalo Jina lako nitalishukuru kwa ajili ya upole wako na kwa ajili ya welekevu wako, kwani umelikuza Jina lako kwa kufanya mambo yapitayo yote, uliyoyasema. Siku, nilipokuita, uliniitikia, ukaishupaza roho yangu na kuitia nguvu. Bwana, wafalme wote wa nchi watakushukuru watakapokuwa wameyasikia maneno, kinywa chako kiliyoyasema. Watakapozishika njia za Bwana wataimba, ya kuwa utukufu wa Bwana ni mkubwa. Kwani Bwana huko juu aliko humtazama mnyenyekevu, lakini mwenye majivuno anamjua, akiwa yuko mbali bado. Kama ninaendelea kusongeka po pote, unanishika moyo, nisizimie; makali ya adui zangu uliyainulia mkono wako. mkono wako wa kuume ukaniokoa. Bwana atanimalizia jambo hili, upole wako, Bwana, ni wa kale na kale. Kazi za mikomo yako usiziache! Bwana, unanichunguza, unanijua. Wewe unajua kukaa kwangu na kuinuka kwangu, ukayatambua mawazo yangu, ijapo uwe mbali. Kma ninakwenda au ninalala, unanivumbua, njia zangu zote zimekuelekea. Kwani hakuna neno, ulimi wangu utakalolisema, usilokwisha kulijua lote, wewe Bwana. Nyuma na mbele umenifungia, ukanibandikia mkono wako. Ni ya kustaajabu, sitaweza kuyatambua, ni mambo makuu, sitaweza kuyafumbua. Nihamie wapi, Roho yako isinijie? Nikimbilie wapi, uso wako usinione? Kama ningekwenda kupaa mbinguni, wewe uko; kama ningekwenda kulala kuzimuni, wewe uko. Kama ningetumia mionzi ya jua kuwa mabawa yangu, nikaja kukaa mapeoni kwenye bahari, huko nako mkono wako ungeniongoza, mkono wako wa kuume ungenishika. Kama ningesema: Giza na liniguie, nao mwanga unizungukao na uwe usiku, giza nalo lisingekuwa lenye weusi machoni pako; maana usiku huangaza kama mchana huko uliko, kwako giza na mwanga huwa sawasawa. Kwani wewe ndiwe uliyeyaumba mafigo yangu, ndiwe uliyeniunga tumboni mwa mama. Ninakushukuru, kwani ni ajabu litishalo, jinsi nilivyotengenezwa, vilivyo kazi zako hustaajabisha kweli, roho yangu inavijua sanasana. Mifupa yangu haikuwa imefichika, usiione, nilipofanyiziwa mahali palipojificha, maana nilitengenezwa mbali sana ndani ya nchi. Nilipokuwa mimba tumboni mwa mama, macho yako yaliniona, nazo siku zangu zote zilikuwa zimeandikwa kitabuni mwako hapo, zilipoambiwa, zitokee; ilikuwa hapo, hata moja yao ilipokuwa haijawa bado. Lakini kwangu ni vigumu sana kuyajua mawazo yako, Bwana, nikiyachanganya, yako na nguvu za kunishinda. Yangekuwa mengi kuliko mchanga, kama ningeweza kuyahesabu. Ningaliko kwako bado ninapoamka. Nakuomba, Mungu, uwaue wasiokucha, wenye manza za damu waondoke kwangu; ndio wanaokutaja tu, wapate kuuficha ukorofi wao; kwa kuwa wabishi wako, hujivuna bure. Wachukizwao na wewe, Bwana, nisiwachukie? Nao wakuinukiao nisitapishwe nao? Ninawachukia kwa uchukivu usiosaza hata kidogo, ninawatazama kuwa adui zangu mimi. Nichunguze, Mungu, uujue moyo wangu! Nijaribu, uyajue nayo mawazo, niliyo nayo! Tazama, kama nimeshika njia iendayo kwenye maumivu, unishikishe njia iendayo kwenye kuwapo kale na kale! Bwana, kwenye watu wabaya niopoe! nilinde, watu wenye makorofi wasinijie! Ndio wanaowaza mabaya mioyoni mwao, nao hufanya magomvi kila siku. Wamezinoa ndimi zao, ziwe kama za nyoka, sumu ya pili imo midomoni mwao. Niangalie, Bwana, mikono yao wasiokucha isinikamate! Nilinde, watu wenye makorofi wasinijie! Ndio wawazao, jinsi watakavyonikumba, nije kujikwaa Wenye majivuno wamenitegea matanzi na nyugwe, wakanitandikia nyavu kandokando ya njia, wakaiweka nayo mitego yao, waninase. Nikamwambia Bwana: Wewe ndiwe Mungu wangu! Bwana, zisikilize sauti za malalamiko yangu! Bwana uliye Bwana wangu mwenye nguvu, u wokovu wangu, unakikingia kichwa changu siku za mapigano. Bwana, wasiokucha usiwape wanayoyatamani! Wala usiwamalizie mashauri yao mabaya, wasijivune! Sumu zao wanizungukao nazo njama zao, walizozisema za kupotoa, na ziwarudie wenyewe na kuwafunika! Na awanyeshee mvua ya makaa ya moto! Na awakumbe, waanguke, motoni namo mashimoni, wasiweze kabisa kuinuka tena! Mtu mwenye masingizio hatashikizwa katika nchi, mtu mwenye makorofi mabaya na yamkimbize, mpaka aangamie! Ninajua, ya kuwa Bwana atamwamulia aliye mnyonge, nayo mashauri ya wakiwa atayanyosha. Watakaolishukuru Jina lako kweli ndio waongofu, nao wanyokao mioyo watakaa usoni pako. Bwana, nimekuita, unijie upesi! Isikilize sauti yangu, nikikuita! Maombo yangu na yapande kufika kwako kama moshi wa uvumba! Kipaji changu cha tambiko cha jioni ni mikono, nikuinuliayo. Bwana, ukiwekee mlinzi hiki kinywa changu, angoje penye huu mlango wa midomo yangu! Usiugeuze moyo wangu kuelekea neno baya, nikijitendea matendo ya kukubeza pamoja nao wafanyao maovu, nisije kula vilaji vyao, ijapo viwe vya urembo! Mwongofu akinipiga, anichape kwa upole! Hivyo vitakuwa kama mafuta ya kupaka kichwa, nacho kichwa changu hakitayakataa. Nami nimo bado katika kuomba kwa ajili ya mabaya yao wale. Waamuzi wao watakapokuwa wameangushwa magengeni, ndipo, watakapoyasikia maneno yangu, ya kuwa ni mazuri. Kama vilivyo hapo, mtu alipolima na kuchimbachimba, ndivyo, mifupa yetu ilivyotawanyika kwenye lango la kuzimu. Kwani wewe, Bwana Mungu, ndiwe unayetazamiwa na macho yangu, nimekukimbilia wewe, usiimwage roho yangu! Niangalie, nisinaswe na tanzi, walilonitegea, wala nisikamatwe na kamba zao wafanyao maovu! Wasiokucha sharti wanaswe wote pamoja na nyavu zao wenyewe, lakini mimi nipe, nizipite kabisa! Napaza zauti, nimlilie Bwana, namlalamikia Bwana na kupaza sauti yangu. Mbele yake nayamwaga machozi yangu, nayo masongano yangu nayatangaza mbele yake yeye. Roho yangu ikitaka kuzimia kifuani mwangu, wewe unaujua mwenendo wangu, jinsi ulivyo. Njiani nipitapo wamenitegea matanzi; ukitazama kuumeni utaona, hakuna anikaguaye. Nimepotelewa na kimbilio, hakuna aniulizaye. Nimekupalizia sauti, Bwana, nikasema kwamba: Wewe u kimbilio langu na fungu langu nchini kwao walio hai. Yaangalie malalamiko yangu! Kwani nimekorofika sana. Niopoe kwao wanikimbizao! Kwani nguvu zao hunishinda. Itoe roho yangu kifungoni, ilishukuru Jina lako! Waongofu watanizunguka, ukinitendea mema. Bwana, sikiliza, nikikuomba, uangalie, nikikulalamikia! kwa kuwa u mwelekevu na mwongofu, na uniitikie! Usije kwa mtumishi wako, upate kumhukumu! Kwani kwao wote walio hai hakuna aliye mwongofu. Kwani adui yangu ameikimbiza roho yangu, akaniponda na kuniangusha chini akitaka kuniua, akanikalisha kwenye giza kama wao waliokufa kale. Roho yangu ikataka kuzimia kifuani mwangu, moyo wangu humu mwilini ukaguiwa na kituko. Nikazikumbuka siku zilizopita kale, nayo matendo yako yote nikayachanganya, mikono yako iliyoyafanya nikayawaza yote. Kisha nikakunyoshea mikono yangu, roho yangu ikakutunukia kama nchi kavu. Bwana, niitikie upesi! Roho yangu imemalizika; usinifiche uso wako, nisije kufanana nao washukao kuzimuni! Unipe kusikia asubuhi mambo ya upole wako! Kwani nimekuegemea. Nijulishe njia, nitakayoishika! Kwani nimekuinulia roho yangu. Niopoe, Bwana, ukinitoa kwao walio adui zangu! Nimekukimbilia, unifunike! Kwa kuwa Mungu wangu nifunze kufanya yakupendezayo! Roho yako njema iniongoze, nishike njia inyokayo! Bwana, kwa ajili ya Jina lako nirudishe uzimani! Kwa ajili ya wongofu wako nitoe katika masongano! Kwa ajili ya upole wako wamalize adui zangu! Waangamize wote waisongao roho yangu! Kwani ni mtumishi wako. Na atukuzwe Bwana aliye mwamba wangu! Ndiye aliyeifundisha mikono yangu kupiga vita, ijue hata kupiga konde kwenye mapigano. Ndiye aniendeaye kwa upole, ni ngome yangu na boma langu. Kwa kuwa ngao yangu na kimbilio langu ndiye aniponyaye, yeye ndiye awashurutishaye walio ukoo wangu, wanitii. Bwana, mtu ndio nini, ukimjua? Mwana wa mtu naye, usipomsahau? Mtu hufanana kuwa kama mvuke, siku zake hupita kama kivuli. Bwana, ziinamishe mbingu zako, utelemke! Iguse milima, itoke moshi! Mulikisha umeme, uwatapanye! Ipige mishale yako, uwastushe! Utume mkono wako toka juu, uniopoe! Kwenye maji mengi uniponye! Nitoe mikononi mwao walio wageni tu! Maana vinywa vyao husema maneno ya bure, mikono yao ya kuume ni yenye uwongo. Mungu, nitakuimbia wimbo mpya pamoja na kukupigia pango lenye nyuzi kumi. Yeye ndiye awapatiaye wokovu nao wafalme, naye mtumishi wake Dawidi humwopoa, upanga mbaya usimpige. Niopoe na kuniponya mikononi mwao walio wageni tu! Maana vinywa vyao husema maneno ya bure, mikono yao ya kuume ni yenye uwongo. Wana wetu wa kiume katika ujana wao tunawaombea, wakue kama miti ya kupandwa iliyotunzwa vizuri! Nao wana wetu wa kike na wawe kama nguzo zilizochorwa vizuri kuwa mapambo yao majumba matukufu. Vichanja vyetu na viwe vimejaa, vipate kutoa vilaji viwavyo vyote! Kondoo wetu na wawe wengi sana wakizaa maelfu na maelfu mashambani kwetu! Ng'ombe wetu na wawe wenye mimba, wasipatwe na kidei wala na mengine yawamalizayo, pasiwe na vilio nyuani petu! Wenye shangwe ni ukoo wa watu wayapatayo yayo hayo. Wenye shangwe ni ukoo wa watu, Bwana akiwa Mungu wao. Na nikutukuze, Mungu wangu, uliye mfalme! Na nilisifu Jina lako kale na kale! Na nikusifu siku zote, nisikome kulishangilia Jina lako kale na kale! Bwana ni mkuu, hushangiliwa sana, ukuu wake hauchunguziki. Kizazi kinasifia kizazi kingine kazi zako na kuyatangaza matendo yako yaliyo makuu. Urembo na utukufu ndio mapambo yako, mambo yako ya kustaajabisha na niyawaze moyoni! Watu na wayaongee ya nguvu zako yaogopeshayo, na niyasimulie matendo yako yaliyo makuu! Na waukumbuke wema wako mwingi, wautangaze, nao wongofu wako waupigie vigelegele! Bwana ni mwenye utu na mwenye huruma, tena ni mwenye uvumilivu na mwenye upole mkubwa. Bwana huwaendea wote kwa kuwa mwema, yote aliyoyafanya huyaonea uchungu. Bwana, kazi zako zote na zikushukuru, nao wakuchao na wakutukuze! Utukufu wa ufalme wako na wauongee! Na wasimuliane matendo yako yaliyo makuu! Hayo matendo yako makuu na wayajulishe wana wa watu, hata utukufu na urembo wa ufalme wako! Ufalme wako ni ufalme wa siku zote za kale na kale, nao ubwana wako ni wa vizazi vyote kwa vizazi na vizazi. Bwana huwashikiza wote waangukao, huwainua wote walioinamishwa. *Macho yao wote hukutazamia, nawe huwapa vilaji vyao, wanapoona njaa. Unapokifumbua kiganja chako, huwashibisha wote waliopo, wapendezwe. Katika njia zake zote Bwana ni mwongofu, katika kazi zake zote ni mwenye upole. Bwana yuko karibu kwao wote wamwitao, kwao wote watakaomwita kwa ukweli. Huyafanya yawapendezayo wamwogopao, huyasikia malalamiko yao, wakimlilia, huwaokoa. Bwana huwalinda wote wampendao, lakini wote wasiomcha atawaishiliza. Kinywa changu sharti kiseme sifa za Bwana! Wote wenye miili ya kimtu sharti walitukuze Jina lake takatifu pasipo kukoma kale na kale!* Haleluya! Mshangilie Bwana, roho yangu! Na nimshangilie Bwana siku zangu za kuwapo! Na nimwimbie Mungu wangu na kupiga zeze nikingali nipo! Msiegemee wakuu! Nao ni wana wa watu, hawawezi kuokoa. Roho ya mtu ikimtoka, inarudi mchangani; siku ile mizungu yake itakuwa imepotea. Mwenye shangwe ni mtu wa Mungu wa Yakobo, maana humsaidia, akimngojea Bwana, Mungu wake. Yeye ndiye aliyezifanya mbingu na nchi, hata bahari navyo vyote vilivyomo. Yeye ndiye ashikaye welekevu na kuufuata kale na kale. Yeye ndiye anayewaamulia waliokorofishwa, yeye ndiye anayewashibisha wenye njaa. Yeye Bwana ndiye anayewafungua waliofungwa, yeye Bwana ndiye anayefumbua macho ya vipofu, yeye Bwana ndiye anayewainua walioinamishwa, yeye Bwana ndiye anayewapenda waongofu, yeye Bwana ndiye anayewaangalia nao wageni, nao waliofiwa na wazazi, hata wajane huwaegemeza, lakini njia yao wasiomcha huipoteza. Bwana anashika ufalme kale na kale, Mungu wako, Sioni, ni wa vizazi na vizazi. Haleluya! Haleluya! kwa kuwa ni vema kumwimbia Mungu wetu, ni vizuri kumshangilia, nako kunapasa. Anayeujenga Yerusalemu ndiye Bwana, nao Waisiraeli waliotawanyika anawakusanya. Yeye anawaponya waliovunjika mioyo, ndiye anayewafunga vidonda vyao, walipoumizwa. Ndiye anayekiweka kiwango cha nyota, zote anaziita majina. Bwana wetu ni mkubwa mwenye nguvu nyingi, matambuzi yake hayahesabiki. Bwana ndiye anayewaegemeza watesekao, tena ndiye anayewakumba wasiomcha, waanguke chini. Mwitikieni Bwana na kumshukuru! Mwimbieni Mungu wetu na kupiga mazeze! Yeye ndiye anayeifunika mbingu kwa mawingu, naye anayezinyeshea nchi mvua ndiye yeye, ndiye anayechipuza majani huko milimani. Yeye ndiye anayewapa nyama vilaji vyao, nao makinda ya kunguru wamliliao. Nguvu kubwa za farasi hazifurahii, wala hapendezwi na miguu ya mtu; Bwana hupendezwa nao wamwogopao, nao wanaoungojea upole wake. Yerusalemu, msifu aliye Bwana! Mshangilie Mungu wako, wewe Sioni! Kwani makomeo ya malango yako anayatia nguvu, anawabariki watoto, ulio nao. Utengemano ndio, anaoipatia mipaka yako, anakushibisha ngano zilizo nzuri kuliko nyingine. Hutuma amri yake kufika katika nchi, maneno yake huendelea upesi sana. Hunyunyiza manyunyu ya theluji, yaking'aa kama pamba, ni wingu la baridi liyamwagalo, yamwagike kama majivu. Mawe ya mvua huyatupa, kama ni kokotokokoto, yuko nani atakayeweza kusimama kwenye baridi hiyo? Lakini akisema neno tu, yanayeyuka, akituma upepo wake, yanageuka kuwa maji, yajiendee. Yeye ndiye anayemtangazia Yakobo maneno yake, nayo maongozi yake na maamuzi yake huwatangazia Waisiraeli. Hivyo hakuvifanyizia wamizimu wo wote, nayo maamuzi yake hakuwajulisha. Haleluya! Haleluya! Mshangilieni Bwana kule mbinguni! Mshangilieni huko juu! Ninyi malaika zake wote, mshangilieni! Ninyi vikosi vyake vyote, mshangilieni Jua na mwezi, mshangilieni! Ninyi nyota zote zenye mwanga, mshangilieni! Mbingu zilizoko juu ya mbingu, mshangilieni pamoja na maji yaliyoko mbinguni juu! Jina la Bwana lishangilieni! Yeye alipoagiza, ziliumbwa. Akazisimamisha za kuwapo kale na kale, akazikatia pao pa kuwapo, zisipapite. Mshangilieni Bwana huku nchini, ninyi nyama wakubwa wa baharini na vilindi vyote! Moto na mvua ya mawe theluji na kungugu, upepo wa kimbunga ulitimizao Neno lake, milima na vilima vyote, ijapo viwe vidogo, miti izaayo matunda na miangati yote, nyama wote wa nyumbani nao wa porini, wadudu pamoja na ndege, wao warukao, wafalme wa nchi na makabila yote ya watu, wakuu wao wote walio waamuzi wa nchi, vijana wa kiume nao wa kike, wazee pamoja nao walio watoto, wote pia na walishangilie Jina la Bwana! Kwani limetukuka peke yake, utukufu wake unaupita wa nchi na wa mbingu. Alipoyaelekeza juu mabaragumu yao walio ukoo wake, ndipo, wote waliomcha walipoyashangilia, wao wana wa Isiraeli walio ukoo wake umkaliao karibu. Haleluya! Heleluya! Mwimbieni Bwana wimbo mpya! Mkutano wao wamchao na umshangilie! Waisiraeli na wamfurahie aliyewafanya! Wana wa sioni na wampigie vigelegele aliye mfalme wao! Na walishangilie Jina lake na kucheza ngoma! Na wamwimbie na kupiga patu pamoja na mazeze! Kwani Bwana anapendezwa nao wlaio ukoo wake, huwaokoa watesekao na kuwapamba vizuri. Wamchao na wapige shangwe kwa kupate utukufu! Na wapige vigelegele katika vilalo vyao! Na wamtukuze Bwana kwa makoo yao! Namo mikononi mwao na washike panga zenye makali pande mbili! Wajipatie malipizi kwao wamizimu, makali ya hao watu wayapatilize! Wawafunge wafalme wao kwa minyororo nao watukufu wao kwa mapingu ya chuma! Wawafanyizie zile hukumu, walizoandikiwa! Macheo kama hayo watapewa wote wamchao. Haleluya! Haleluya! Mshangilieni bwana hapo Patakatifu pake! Bomani mwake mwenye nguvu mshangilieni! Kwa ajili ya matendo yake ya nguvu mshangilieni! Kwa ajili ya ukuu wake mwingi mshangilieni! Kwa kuvumisha mabaragumu mshangilieni! Kwa kupiga mapango na mazeze mshangilieni! Kwa kupiga patu na kucheza ngoma mshangilieni! Kwa kupiga vinanda na mazomari mshangilieni Kwa kupiga matoazi yaliayo vizuri mshangilieni! Kwa kupiga matoazi yenye mavumo sana mshangilieni! Na wamshangilie Bwana wote wenye pumzi! Haleluya! Waje kujua werevu wa kweli na kuonyeka, wajue kutambua maneno ya utambuzi, waje kuonyeka, wapate akili, tena wapate wongofu na mashauri mema yaongokayo, waerevushe wajinga, nao wavulana wawajulishe kuwaza mambo mioyoni! Naye mwerevu wa kweli ayasikie, auongeze ujuzi wake, naye mtambuzi ajipatie wongozi mwema. atambue mifano na vitendawili, hata maneno ya werevu wa kweli na mafumbo yao! Kumcha Bwana ndio mwanzo wa ujuzi, lakini wajinga huubeza werevu wa kweli kwa kukataa kuonyeka. Mwanangu, sikia, baba yako akikuchapa, usiyabeue maonyo ya mama yako! Kwani hayo ni kilemba kipendezacho kichwani pako na mkufu wa pambo shingoni pako. Mwanangu wakosaji wakikubembeleza, usiwaitikie! Wakikuambia: Twende pamoja, tuvizie kumwaga damu, tena tumwotee bure asiyekosa, kama kuzimu tuwameze, wakingali wa hai, wao wamchao Mungu wawe kama wengine washukao shimoni, tuzipate mali zao zote zenye kima, tuzijaze nyumba zetu mateka, kisha nawe utapiga kura pamoja nasi, sisi sote pia tutakuwa bia moja tu: mwanangu, hao usishike njia moja nao, uzuie mguu wako, usikanyage mikondo yao! Kwani miguu yao hukimbilia mabaya, hupiga mbio kuja kumwaga damu. Ni bure, wavu ukiwa umetandwa machoni pao wote walio wenye mabawa. Hivyo wao huvizia kumwaga damu zao wenyewe na kuziotea roho zao wenyewe. Ndivyo, zilivyo njia zao wote wanaotamani mali tu, maana giza huzichukua roho zao wenyewe. Werevu wa kweli hupiga mbiu barabarani, huipaza sauti yake viwanjani; hutangaza pembeni penye njia pasipo na makelele mengi, napo pa kuingia malangoni, namo mjini husema maneno yake: Mpaka lini mtayapenda mapumbavu, ninyi wapumbavu? nanyi wafyozaji mtapendezwa na ufyozaji mpaka lini? nanyi wajinga mtauchukia ujuzi mpaka lini? Geukeni kwa kuonywa na mimi! Mtaniona, nikiwamwagia roho yangu, nikiwajulisha maneno yangu. Kwa kuwa niliwaita, mkakataa kunisikia, kwa kuwa niliukunjua mkono wangu, lakini hakuwako aliyeuangalia, mkayaacha mashauri yangu yote, hamkutaka kuonywa na mimi: kwa hiyo mimi nami nitacheka, mkiangamia, nitawasimanga, mastuko yatakapowajia; hayo mastuko yatawajia kama mvua yenye umeme, nao mwangamizo utawatukia kama upepo wa kilazoni, nayo masongano na mahangaiko yatawajia. Hapo ndipo, watakaponiita, lakini sitawaitikia, watanitafuta kwa bidii tangu asubuhi, lakini hawataniona. Kwa kuwa waliuchukia ujuzi, hawakutaka kumcha Bwana, wala hawakuyapenda mashauri yangu, wakakataa po pote kuonywa na mimi, kwa hiyo watayala mazao ya njia zao, wayashibe mashauri yao. Kwani kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, nako kujikalia tu kwao wapumbavu kutawaangamiza. Lakini atakayenisikia atakaa na kutulia, atatengemana pasipo kuona kibaya kitakachomstusha. *Mwanangu, ukiyapokea maneno yangu na kuyashika maagizo yangu moyoni mwako, ukiutegea werevu wa kweli sikio lako, ukauelekezea utambuzi moyo wako, ukiziita akili na kuipaza sauti yako, upate utambuzi, ukiutafuta, kama unavyotafuta fedha, ukiuchunguza, kama unavyochunguza mali zilizofichwa: ndipo, utakapoitambua maana ya kumcha Bwana, tena ndipo, utakapopata kumjua Mungu. Kwani Bwana huerevusha kweli, kinywani mwake hutoka ujuzi na utambuzi. Wanyokao aliwawekea wokovu, ni ngao yao waendeleao pasipo kukosa, ayalinde mapito yaliyo sawa na kuzingalia njia zao wamchao.* Ndipo, utakapotambua wongofu na mashauri yaliyo sawa nayo yanyokayo na kila njia njema, kwani werevu wa kweli utaingia moyoni mwako, nao ujuzi utaupendeza roho yako. Mawazo mema ya moyo yatakuangalia, nao utambuzi utakulinda, yakuponye, usiishike njia ya wabaya, usiwafuate watu wasemao mapotovu, walioziacha njia zinyokazo, waende katika njia zenye giza. Wanaofurahiwa na kufanya mabaya, wanaoshangilia mapotovu ya wabaya, njia zao nazo ni za upotovu, nayo mikondo yao hainyoki. Nayo yale mawazo mema ya moyo yatakuponya, usimchukue mwanamke mgoni aliye wa mwingine, ijapo akubembeleze kwa maneno mazuri; kwa kuwa alimwacha mpendwa wa ujana wake na kulisahau agano la Mungu wake, nyumba yake inatumbukia penye kifo, nayo mapito yake humwongoza kwenda kwao wazimu. Wote walioingia mwake hakuna atakayerudi, wala hakuna atayezifikilia njia za kwenda uzimani. Huku na kwamba: Uende katika njia ya watu wema na kuyashika mapito yao walio waongofu. Kwani wanyokao ndio watakaokaa katika nchi, nao wamchao Mungu watasazwa huku; lakini wasiomcha Mungu watang'olewa katika nchi, nao waliomwacha Bwana watapokonywa huku. Mwanangu, usiyasahau maonyo yangu! Nao moyo wako na uyalinde maagizo yangu! Kwani yatakupatia siku nyingi na miaka mingi ya kukaa mwenye uzima na mwenye utengemano. Upendo wa kweli usikuache, uufunge shingoni pako, tena uuandike katika kibao cha moyo wako! Ndivyo, utakavyoona upendeleo na akili njema machoni pake Mungu napo machoni pa watu. Mjetee Bwana kwa moyo wako wote, usijiegemeze utambuzi wako! Katika njia zote umjue yeye! Ndivyo, atakavyokunyoshea mapito yako. Usijiwazie mwenyewe kuwa mwenye werevu wa kweli, ila umche Bwana, uepuke penye mabaya! Hii itakuwa dawa ya kitovu chako na kunywaji cha kuitia mifupa yako nguvu. Mheshimu Bwana ukimtolea vipaji vya mali zako na malimbuko ya mapato yako yote! Ndipo, vyanja vyako vitakapojazwa, nayo makamulio yako yatafurikiwa na pombe mbichi. Mwanangu, usiseme: Si kitu, ukichapwa na Bwana! Wala usilegee, unapokanywa naye! Kwani Bwana humchapa anayempenda, kama baba anavyomchapa mwanawe ampendezaye. Mwenye shangwe ni mtu aonaye werevu wa kweli, naye mtu apataye utambuzi, kwani kuupata ni kwema kuliko kupata fedha, nayo faida yake ni kubwa kuliko dhahabu tupu; maana una kima kuliko lulu, nayo yote pia yapendezayo watu hayalingani nao. Siku nyingi za kuwapo zimo kuumeni mwake, namo kushotoni mwake umo utajiri na utukufu. Njia zake ni njia za kupendeza, nayo mikondo yake ni yenye utengemano. Ndio mti wenye uzima kwao walioushika, mwenye shangwe ni mtu anayeshikamana nao. Bwana aliuweka msingi wa nchi kwa werevu wa kweli, nazo mbingu alizishupaza kwa utambuzi. Kwa ujuzi wake vilindi vya maji vikatokea kuwa mboji, nayo mawingu hudondoka umande. Mwanangu, haya yasitoweke machoni pako! uangalie ujuzi wa kweli na mawazo ya moyo! Ndivyo, utakavyoipatia roho yako uzima, tena utakuwa pambo zuri shingoni pako. Ndivyo, utakavyokwenda katika njia yako na kutulia, nao mguu wako hautajikwaa. Utakapolala hutapatwa na woga, kweli utakapolala, usingizi wako utakuwa mtamu, usiyaogope mastusho yatakayokutukia, wala mwangamizo wao wasiomcha Mungu utakapotimia. Kwani Bwana atakuwa egemeo lako, ataulinda mguu wako, usinaswe. Chema cho chote usimnyime mwenzio apaswaye nacho, ikiwa, mkono wako unaweza kumpatia. Usimwambie mwenzio: Nenda, urudi! nitakupa kesho, nawe hicho cha kumpa unacho hapo hapo! Usiwaze kumfanyizia mwenzio mabaya, yeye akikaa na wewe pasipo kuogopa kitu! Usigombane na mtu bure tu, kama hakukufanyizia kibaya! Mkorofi usimwonee wivu, wala njia zake usizichague kuwa za kuzishika! Kwani mpotovu humtapisha Bwana, lakini wanyokao ndio, ambao anakula njama nao. Kiapizo cha Bwana huzikalia nyumba zao wasiomcha, lakini makao ya waongofu huyabariki. Akijia wafyozaji huwafyoza naye, lakini wanyenyekevu huwapatia huruma. Werevu wa kweli watapata utukufu, uwe fungu lao, lakini matukuzo yao wapumbavu ndio matwezo yatakayowapata. Wanangu, sikieni, baba akiwakanya! Yategeni masikio, myajue yenye utambuzi! Kwani ninawapa ninyi mafundisho mema: maonyo yangu msiyaache! Kwani nami nilipokuwa mwana wa baba yangu, mtoto mnyonge aliyependwa sana na mama kwa kuwa wa pekee, baba alinifundisha, akaniambia: Moyo wako sharti uyashike sana maneno yangu, uyaangalie maagizo yangu! Ndipo, utakapopata uzima. Jipatie werevu wa kweli! Jipatie nao utambuzi! Usiusahau! wala usiyageukie mgongo maneno ya kinywa changu! Usiuache! Ndipo, nao utakapokuangalia; uupende! Ndipo, nao utakapokulinda. Mwanzo wa werevu wa kweli ndio huu: jipatie werevu wa kweli! Jipatie utambuzi kwa kuyatoa mapato yako yote! Uutukuze! Ndipo, nao utakapokutukuza, utakupatia macheo, ukiukumbatia. Kichwa chako utakivika kilemba kipendezachao, utakugawia taji yenye utukufu. Sikia, mwanangu, uyapokee maneno yangu! Ndipo, miaka yako ya kukaa uzimani itakapokuwa mingi. Nimekuongoza katika njia ya werevu wa kweli, nikakuendesha katika mapito yanyokayo; ukiyashika, nyayo zako hazitasongeka, hata utakapopiga mbio hutajikwaa. Yashike kwa nguvu mafundisho yakuonyayo, usiyaache kabisa! Yalinde, kwani ndiyo yaliyo uzima wako. Mapito yao wasiomcha Mungu usiyakanyage! Wala usitembee katika njia ya wabaya! Ondoka hapo, ilipo, usiifuate! Epuka hapo, ilipo, upapite! Kwani hawawezi kulala wasipokwisha kufanya mabaya; usingizi huwapotelea, wasipokwisha kukwaza mtu. Kwani vilaji, wanavyovila, ni vya kumbeza Mungu, nayo mvinyo, wanayoinywa, ni yenye makorofi. Lakini mapito ya waongofu huwa kama mwanga wa kucha, huendelea ukiangaza, hata mchana wenyewe utimie. Njia yao wasiomcha Mungu huwa kama giza lenyewe, wasijue, kama ni kitu gani kiwakwazacho. Mwanangu, yasikilize maneno yangu Yategee sikio, ninayokuambia! Usiyaache, yatoweke machoni pako! Yaangalie moyoni mwako ndani! Kwani hayo ndio uzima wao wayapatao, tena ni dawa ya miili yao wote. Kuliko yote, unayoyaanglia, ulinde moyo wako! Kwani humo ndimo, uzima unamotoka. Ondoa kwako upotovu wa kinywa, ukiiepusha midomo yako kwenye mambo yasiyonyoka! Yaelekeze macho yao kuyatazama yaliyoko mbele, kope zako nazo ziyaelekee sawasawa yaliyoko mbele yako! Miguu yako ishikishe mapito yaliyo malinganifu, njia zako zote ziwe zimeshupaa! Usigeukie kuumeni wala kushotoni, upate kuiondoa miguu yako penye mabaya! Mwanangu, usikilize werevu wangu ulio wa kweli! Utegee utambuzi wangu sikio lako, upate kuyaangalia mawazo ya moyo, midomo yako nayo iulinde ujuzi! Kwani midomo ya mwanamke mgeni hudondosha asali, kinywa chake nacho huteleza kuliko mafuta. Lakini mwisho hutokeza uchungu ulio mkali kuliko wa shubiri, hukata kuliko upanga wenye makali pande mbili. Miguu yake hushukia kifo, kuzimuni ndiko, mwenendo wake unakoelekea, asiishike njia iendayo uzimani iliyo sawa, wala asijue, jinsi mapito yake yanavyopotea. Sasa wanangu, nisikieni! Msiyaache maneno ya kinywa changu! Iangalie njia yako, impitie mbali, usipafikie karibu pa kuingia nyumbani mwake, usiwape wengine yaliyo utukufu wako, wala miaka yako isikatwe na mtu asiyeona huruma! Wageni wasijishibishe mali zako, nguvu yako ilizokupatia, wala mapato, uliyoyasumbukia, yasipelekwe nyumbani mwa wengine! Mwisho ukikufikia, utapiga kite; nyama na nguvu za mwili wako zitakapokuwa zimeishilizwa, ndipo, utakaposema: Kumbe nilichukizwa nilipoonywa, moyo wangu ukakataa kuchapwa! Sikuzisikia sauti za wafunzi wangu, wala sikuwategea sikio langu walionifundisha. Ikasalia kidogo, wote mzima nikashikwa na mabaya, nilipokuwa katikati ya mkutano wao wakatao mashauri. Yanywe maji ya shimo lako wewe, nayo maji yabubujikayo katika kisima chako! Je? Chemchemi zako zitawanyike nje? navyo vijito vya maji vitawanyike viwanjani? La, sharti maji yao yawe yako peke yako, yasiwe ya wageni pamoja na wewe! Kisima chako na kibarikiwe, upate kufurahia mke wa ujana wako! Anafanana na kulungu mke apendezaye, tena na paa mke afurahishaye, maziwa yake yakuchangamshe siku zote, kwa upendo wake na uwe pasipo kukoma kama mtu alewaye. Mwanangu, mbona unataka kujilewesha kwa mwanamke mgeni? Mbona unataka kukumbatia kifua cha mwanamke wa mwingine? Kwani machoni pa Bwana njia za kila mtu ziko waziwazi, yeye ndiye anayeyatengeneza mapito ya kila mtu. Manza, alizozikora mwenyewe, zitamnasa asiyemcha Mungu, akamatwe na kamba za makosa yake. Huyo atakufa, kwa kuwa hakuonyeka, kwa ujinga wake mwingi atapepesuka, aanguke. Mwanangu, kama umejitoa kuwa dhamana ya mwenzio, ukampa mwingine mkono wako, kama umejifunga kwa maneno ya kinywa chako, ukanaswa na maneno ya kinywa chako, basi, mwanangu, fanya hivi, upate kujiokoa, kwa kuwa umejitia mkononi mwa mwenzio: nenda kumwangukia mwenzio na kumlalamikia! Usiache, macho yako yalale usingizi, wala kope zako zisinzie! Ponyoka mkononi mwake kama paa, au kama ndege anavyoponyoka mkononi mwa mtega tanzi! Nenda kwao siafu, wewe mvivu, uzitazame njia zao, uerevuke kweli! Hao hawana mkuu wala msimamizi, wala mtawalaji hawana. Hujitengenezea pamba za siku za vuli, hulimbika vyakula penye siku za mavuno yao. Wewe mvivu, unataka kulala mpaka lini? utaamka lini katika usingizi wako? Unataka kulala bado kidogo na kupumzika bado kidogo na kukunja mikono kitandani bado kidogo. Kisha umaskini utakujia kama mpiga mbio pamoja na ukosefu ulio kama mtu aliyevaa mata. Mtu asiyefaa kitu, mtu mwenye maovu ndiye atembeaye mwenye upotovu wa kinywa. Hukonyeza kwa macho yake, huparapara kwa miguu yake, tena hupungia watu kwa vidole vyake. Huwaza mapotovu moyoni mwake akitunga mabaya pasipo kukoma, huchokoza, agombanishe watu. Kwa hiyo mara mwangamizo wake utamjia, asipoviwazia atavunjwa, asione atakayemponya. Yako mambo sita yamchukizayo Bwana, tena yako mambo saba yauchafuaye moyo wake: macho yenye majivuno, ulimi wenye uwongo, mikono imwagayo damu ya mtu asiyekosa, moyo utungao maneno maovu, miguu ipigayo mbio kukimbilia penye mabaya, shahidi ya uwongo asemaye ya kuongopa naye achokozaye, agombanishe ndugu. Mwanangu, lilinde agizo la baba yako, wala usiyabeue maonyo ya mama yako! Yafunge siku zote moyoni mwako, kayavae shingoni pako! Ukitembea, na yakuongoze! Ukilala na yakulinde, ukiamka, na yaongee na wewe! Kwani hilo agizo ni taa, hayo maonyo nayo ni mwanga, ni njia ya kwenda uzimani, ukionyeka kwa kukanywa nayo. Yakuangalie, usitazame mwanamke mbaya, wala usiyasikilize maneno yatelezayo ya mwanamke mgeni! Usiutamani uzuri wake moyoni mwako! wala asikunase na kukukonyeza kwa kope za macho yake! Kwani kwa ajili ya mwanamke mgoni mtu hutoa mali, mpaka akose hata kipande cha mkate; naye mwanamke wa mwingine huotea, mpaka aipate nayo roho ya mtu isiyolipika. Je? Mtu anaweza kupaa moto, auweke kifuani pake pasipo kuzichoma nguo zake? Au mtu anaweza kukanyaga makaa yenye moto, nyayo zake siziungue? Ndivyo, mtu alivyo akiingia kwa mke wa mwenziwe, kwao wote wamgusao hakuna atokaye pasipo kukora manza. Watu hawambezi mwizi aibiaye kujishibisha tu, kama alikuwa na njaa. Akikamatwa hulipa mara saba, ijapo atoe mali zote, alizo nazo nyumbani. Mtu akivunja unyumba na mke wa mwingine amepotelewa na akili, maana hujiangamiza mwenyewe kwa kufanya hivyo. Hupata mapigo na matusi, wala hakuna awezaye kuyafuta yaliyomtia soni. Kwani wivu ni kama moto wa mtu wa kiume, haoni huruma anapojilipiza. Hatazami kabisa makombozi yo yote, ingawa mtolee matunzo mengi, hayataki. Mwanangu, yaangalie maneno yangu, uyashike sana maagizo yangu moyoni mwako! Yaangalie maagizo yangu! Ndipo, utakapopata uzima; yaangalie maonyo yangu, kama unavyoangalia mboni ya jicho lako! Yafunge vidoleni pako, tena yaandike katika kibao cha moyo wako! Uuambie werevu wa kweli: Wewe ndiwe umbu langu, utambuzi nao uuite: Mpendwa wa kujuana naye! Ukuanglie, usitazame mwanamke mgeni, wala usiyasikilize maneno yatelezayo ya mke wa mwingine! Kwani dirishani nyumbani mwangu siku moja nilipochungulia penye vyuma vyake, niliwatazama wajinga, nikaona kijana mmoja aliyepotelewa na akili, nikamtambua katikati yao wasioyajua bado mambo hayo. Alitembea barabarani hapo pembeni, yule alipokaa, akaishika njia ya kutembea penye nyumba yake; ikawa jioni, jua lilipokwisha kuchwa, hata ikawa usiku wa manane penye giza. Mara mwanamke anakuja kukutana naye, alivaa nguo kama mgoni, nao moyo wake ulikuwa mdanganyifu. Anapiga kelele pasipo kujizuia, miguu yake haipendi kukaa nyumbani mwake; mara moja yuko barabarani, mara nyingine yuko uwanjani, huvizia po pote penye njia panda. Basi, huyu akamshika, akamnonea, akaushupaza uso wake akamwambia: Sina budi kutoa kipaji cha tambiko cha shukrani, leo hivi ninavilipa viapo vyangu. Kwa hiyo nimetoka nyumbani, nikutane na wewe, nikauchungulia uso wako, mpaka nikakuona. Kitanda changu nimekitandika mazulia na mablanketi mororo yenye rangi ya Kimisri. Pangu pa kulalia nimepamwagia manukato, manemane na liwa na dalasini. Haya! Njoo, tulileweshe na kukumbatiana hata asubuhi tukifurahishana kwa mapendano! Kwani mume hayumo nyumbani mwake, amekwenda safari, yuko mbali; akachukua mfuko wa fedha mkononi mwake, siku ya mwezi mpevu atarudi nyumbani mwake. Hivyo ndivyo, alivyomshinda kwa maneno yake mengi yatelezayo, akamwangusha kwa huo utelezi wa midomo yake. Mara akamfuata kama ng'ombe aendaye kuchinjwa, kama mwenye wazimu aendaye kufungwa kwa kongwa, mpaka mshale uyachome maini yake; ni kama ndege akimbiliaye tanzi pasipo kujua, ya kuwa anakwenda kuuawa. Sasa wanangu, nisikieni, yategeeni maneno yangu masikio yenu! Uangalie moyo wako, usizielekee njia zake, nawe usije kupotea penye mapito yake! Kwani wengi aliwaangusha alipokwisha kuwatia vidonda, wote waliouawa naye ni wengi sana. Kuingia mwake ni kushika njia za kwenda kuzimuni zitelemkazo kukufikisha penye vyumba vya kifo. Sikilizeni! Werevu wa kweli unawaita, utambuzi nao unapaza sauti yake. Kileleni juu ya vilima, njia zinapofika, penye njia panda ndipo, unaposimama. Napo penye malango ya kutokea mjini, hata penye milango ya kuingia unatangaza kwamba: Ninyi waume ninawaita, ninawapalizia sauti, ninyi wana wa Adamu. Msipojua kitu, utambueni ubingwa! Nanyi wapumbavu itambueni mioyo! Sikilizeni! Kwani nitasema mambo makuu, nikifumbua midomo yangu, yatatoka maneno yanyokayo. Kwani kinywa changu kitayatamka yaliyo ya kweli, maneno yasiyomcha Mungu huitapisha midomo yangu. Maneno yote ya kinywa changu yanaongoka, hakuna hata moja lililopotoka la kudanganya watu. Yote pia humwelea mwenye utambuzi, nao wenye ujuzi huona, ya kuwa yamenyoka. Yapokeeni mafunzo yangu, mwache fedha! Maana ujuzi una kima kuliko dhahabu zilizochaguliwa. Kwani werevu wa kweli ni mwema kuliko lulu, nayo yote pia yapendezayo watu hayalingani nao. Mimi werevu wa kweli ninakaa pamoja na ubingwa, nikapata kujua nayo mawazo ya moyo. Kumcha Bwana ni kuyachukia mabaya; kujikuza kujivuna na kushika ufalme wao, na kusema mapotovu ndiko, ninakochukia. Ninayo mashauri mema na ujuzi wa kweli, tena ninao utambuzi na uwezo. Kwa msaada wangu wafalme hushika ufalme wao, nao wakuu hutoa maongozi yaongokayo. Kwa msaada wangu watawalaji hutawala, nao mabwana wakubwa na waamuzi wote wa nchi. Wanipendao ninawapenda, nao wanitafutao kwa bidii toka asubuhi huniona. Mali na macheo ninayo, hata malimbiko yenye utukufu na mtendo yaongokayo. Mazao yangu ni mema kuliko dhahabu, ijapo ziwe zimetakata sana; mtu anayoyapata kwangu ni mema kuliko fedha zilizochaguliwa. Ninashika njia iongokayo, nikapitia katikati palipo sawa, niwapate mali wao wanipendao na kuzijaza vyanja vyao. Bwana aliniumba, niwe mwanzo wa njia yake, hapo kale kabisa, alipokuwa hajatengeneza vingine; nikawekwa kuwapo tangu kale, tangu mwanzo, ulimwengu ulipokuwa haujawa bado. Vilindi vilipokuwa havijawa bado, nilikuwa nimezaliwa, nazo chemchemi zibubujikazo maji zilikuwa hazijawa bado. Milima ilipokuwa haijawekewa misingi, navyo vilima vilipokuwa havijawa bado, nilikuwa nimezaliwa. Alipokuwa hajaiumba nchi na mbuga, nao mwanzo wa mavumbi ulipokuwa haujawa bado, alipozishikiza mbingu, ndipo, nilipokuwa naye, ilikuwa hapo, alipoupima mviringo wake juu ya vilindi vya maji. Alipoyashupaza mawingu huko juu, visima vilivyoko vilindini viliposongana kwa nguvu, alipoikatia bahari mipaka yake, maji yake yasipite hapo, aliposema, alipoishupaza nayo misingi ya nchi: ndipo, nilipokuwa kwake kuzitazama kazi hizo, nikawa mwenye furaha siku kwa siku nikicheza mbele yake siku hizo zote. Nikacheza katika nchi yake, ilipokaa watu, nikawafurahia hao watu. Sasa wanangu, nisikilizeni! Wenye shangwe ndio wazishikao njia zangu. Yasikieni mafunzo, mpate kuerevuka kweli! Msiyaache kabisa! Mwenye shangwe ni mtu anisikiaye, alalaye macho siku kwa siku penye malango yangu. Kwani aliyenipata mimi amekwisha kupata uzima, tena huona upendeleo kwake Bwana. Lakini asiyenipata mimi huikorofisha roho yake mwenyewe, kwani wote wanichukiao hupenda kufa. *Werevu wa kweli ulijenga nyumba yake, ukazichonga nguzo zake saba. Ukachinja nyama wake, ukaziandalia mvinyo zake, ukatandika nayo meza yake. Kisha ukatuma vijakazi wake kualika wageni mjini po pote palipoinukia kwamba: Aliye mjinga aje kuingia humu! Nao wasiojua kitu ukawaambia: Njoni, mle vilaji vyangu! Nyweni nazo mvinyo, nilizoziandalia! Ninyi wajinga, uacheni ujinga, mpate uzima, mwendelee katika njia ya utambuzi! Amkanyaye mfyozaji hujipatia matusi, naye aonyaye mtu asiyemcha Mungu hutiwa soni naye. Usimwonye mfyozaji, asikuchukie! Mwonye mwerevu wa kweli naye atakupenda. Aliye mwerevu wa kweli mwerevushe, ndipo, atakapoendelea kuerevuka zaidi. Aliye mwongofu mfunze! Ndipo, atakapoendelea kujipatia ujuzi. Kumcha Bwana ndio mwanzo wa werevu wa kweli, tena kumjua Mtakatifu ndio ujuzi.* Kwani kwa msaada wangu siku zako zitakuwa nyingi, nayo miaka yako ya kukaa mwenye uzima itaongozeka. Ukiwa umeerevuka kweli, umejipatia mapato ya werevu wa kweli; ukiwa u mfyozaji, basi, utatwikwa peke yako huo mzigo wako. Mwanamke aitwaye ujinga hupiga kelele; yeye aliye mjinga asiyejua maana ya kitu cho chote hukaa mlangoni pa nyumba yake katika kiti mahali pa mjini panapoinukia, awaalike wote wapitao njiani nao wanaokwenda katika njia zao zinyokazo, akisema: Aliye mjinga aje kuingia humu! Nao wasiojua kitu huwaambia: Maji yaliyoibiwa ni matamu, navyo vilaji vinavyoliwa na kufichaficha hupendeza! Naye mjinga hajui, ya kuwa ndiko, mizimu iliko, ya kuwa wao walioalikwa naye hufika katika makorongo ya kuzimuni. Mwana mwerevu wa kweli humfurahisha baba yake, lakini mwana mpumbavu humpatia mama yake majonzi. Malimbiko yaliyopatwa kwa uovu hayafai kitu, lakini wongofu huponya kufani. Bwana hatamwacha mwongofu, afe kwa njaa, lakini tamaa zao wasiomcha huzikumba. Afanyaye kazi na kulegeza mikono hapati kitu, lakini mikono yao wajihimizao hupata mali. Avunaye siku za kipupwe ni mwenye akili, lakini alalaye siku za mavuno hujipatia soni. Mbaraka hukikalia kichwa cha mwongofu, lakini vinywani mwao wasiomcha Mungu yamo makorofi. Ukumbuko wa mwongofu huleta mbaraka, lakini majina yao wasiomcha Mungu huoza. Mwerevu wa moyo huonyeka, lakini mjinga anayejisemea tu hujiangamiza. Aendeleaye pasipo kukosa huenda na kutulia, lakini azipotoaye njia zake hujulikana. Akonyezaye kwa jicho hukasirisha, naye mjinga anayejisemea tu hujiangamiza. Kinywa cha mwongofu ni kisima cha uzima, lakini vinywani mwao wasiomcha Mungu yamo makorofi. Uchukivu huleta magomvi, lakini upendo huyafunika makosa yote. Midomoni mwake mtambuzi huoneka werevu wa kweli, lakini apotelewaye na akili hupaswa na fimbo mgongoni. Werevu wa kweli hulimbika ujuzi, lakini kinywa chake mjinga ni mwangamizo ulio karibu. Mali zake mkwasi ni boma lake lenye nguvu, lakini ukosefu wao wanyonge kuwalegeza mioyo. Kazi yake mwongofu humwelekeza penye uzima, lakini mapato yake asiyemcha Mungu humkosesha. Aangaliaye akikanywa yumo katika njia ya kwenda uzimani, lakini akataaye maonyo hujipoteza. Mwenye uchukivu moyoni husema madanganyifu, naye aenezaye masingizio ni mpumbavu. Asemaye maneno mengi hakosi kuwa mpotovu, lakini ajuaye kuizuia midomo yake ni mjuzi kweli. Ulimi wa mwongofu ni fedha zilizochaguliwa, lakini mioyo yao wasiomcha Mungu haina kima. Midomo ya mwongofu hulisha wengi, lakini wajinga hufa kwa kupotelewa na akili. Mbaraka ya Bwana huwapatia watu mali, lakini masumbuko ya mtu hayaziongezi kamwe. Kwake mpumbavu ni kama mchezo kufanya mabaya, ayawazayo moyoni, lakini mtu mwenye utambuzi hufanya yenye werevu wa kweli. Asiyemcha Mungu anayoyaogopa, ndiyo yanayomjia, lakini waongofu hupewa wayatakayo. Upepo mkali unapopitia, asiyemcha Mungu hayupo tena, lakini mwongofu anao msingi wa kale na kale. Kama siki inavyoyatendea meno na kama moshi unavyoyatendea macho, ndivyo, mvivu anavyowatendea waliomtuma. Kumcha Bwana huziongeza siku za kuwapo, lakini miaka yao wasiomcha Mungu hukatwa. Kungojea kwao waongofu hugeuka kuwa furaha, lakini matumaini yao wasiomcha Mungu hupotea. Njia ya Bwana ni ngome yake amchaye Mungu, lakini ni mwangamizo wao wafanyao maovu. Mwongofu hatukusiki kale na kale, lakini wasiomcha Mungu hawatakaa katika nchi. Kinywa cha mwongofu huchipuza yenye werevu wa kweli, lakini ulimi usemao mapotovu utang'olewa. Midomo ya mwongofu huyajua yapendezayo, lakini vinywa vyao wasiomcha Mungu hujua mapotovu. Mizani ya kudanganyia humtapisha Bwana, lakini mawe ya sawasawa ya kupimia humpendeza. Majivuno yanapofika, ndipo, matusi yanapofika nayo, lakini werevu wa kweli huwakalia wanyenyekevu. Utawa wao wanyokao mioyo huwaongoza, lakini waliomwacha Mungu upotovu wao huwaangamiza. Mali hazifai kitu siku, makali yanapotokea, lakini wongofu huponya hata kufani. Wongofu wao wamchao Mungu huzinyosha njia zao, lakini asiyemcha Mungu ataangushwa na uovu wake. Wongofu wao wanyokao mioyo utawaponya, lakini waliomwacha Mungu watanaswa na tamaa zao. Mtu asiyemcha Mungu anapokufa, kingojeo chake hupotea, nayo matumaini yao wapotovu hupotea. Mwongofu hutolewa katika masongano, lakini asiyemcha Mungu hutiwa mahali pake. Mpotovu humwangamiza mwenziwe kwa kinywa chake, lakini waongofu huokolewa kwa ujuzi wao. Waongofu wakipata mema, mji huwashangilia, lakini wasiomcha Mungu wakiangamia, watu huwazomea. Kwa mbaraka yao wanyokao mji hutukuka, lakini kwa ajili ya vinywa vyao wasiomcha Mungu hubomolewa. Ambezaye mwenziwe amepotelewa na akili, lakini mtu mwenye utambuzi hunyamaza. Atembeaye na kusingizia hufunua mashauri ya njama, lakini mwenye moyo mwelekevu huficha mambo kama hayo. Pasipo wongozi mwema ukoo mzima wa watu huanguka; huokoka, wenye mashauri mema wakiwa wengi. Aliyejitoa kuwa dhamana ya mgeni atapatwa na mabaya zaidi, lakini akataaye kumpa mwingine mkono hukaa na kutulia. Mwanamke apendezaye kujipatia heshima, lakini wakorofi hujipatia mali nyingi. Mtu mwenye huruma hujifanyizia mema mwenyewe, lakini asiye na huruma hujiumiza mwili wake. Asiyemcha Mungu hujipatia mali za udanganyifu, lakini apandaye yenye wongofu hujipatia mshahara wa kweli. Wongofu unapeleka uzimani kweli, lakini ayakimbiliaye mabaya huenda kufani. Wenye mioyo mapotovu humtapisha Bwana, lakini washikao njia zisizo za ukosaji humpendeza. Ingawa wapeane mikono, mbaya hana budi kupatilizwa, lakini wazao wao waongofu watapona. Mwanamke mzuri asiye na akili ni pete ya dhahabu puani mwa nguruwe. Tamaa za waongofu hutamani mema tu, lakini wasiomcha Mungu wanayoyangojea, huwapatia makali. Mwingine hujipatia mali zaidi kwa kugawia wengine, lakini mwingine huzidi kukosa mali, ijapo aziweke kupita kiasi. Apendaye kugawia hushibishwa mwenyewe, anyweshaye wengine naye hunyweshwa. Anyimaye wenzake ngano watu humwapiza, lakini mbaraka hukifia kichwa chake aziuzaye. Atafutaye mema toka asubuhi hupendeza, lakini atafuataye mabaya, yayo hayo humrudia mwenyewe. Azitumainiye mali zake huangushwa nazo, lakini waongofu huchapuka kama majani. Awavurugaye wa nyumbani mwake hujipatia upepo, uwe fungu lake, mpumbavu sharti amtumikie mwenye moyo mwerevu wa kweli. Mazao ya mwongofu ni mti wa uzima, mwerevu wa kweli huzishinda roho za watu. Tazameni! Mwongofu hupata mshahara wake katika nchi hii, Tena itakuwaje? Asiyemcha Mungu na mkosaji asilipishwe zaidi? Apendaye kuonywa hupenda ujuzi, lakini achukiaye kukanywa hupumbaa kama nyama. Mwema hujipatia upendeleo kwake Bwana, lakini mwenye mawazo mabaya humpatiliza. Hakuna atakayeshupaa vema kwa kuacha kumcha Mungu, lakini mashina ya waongofu hayatang'oleka. Mwanamke mwema ni kilemba cha mumewe, lakini ampatiaye soni ni kama ugonjwa wa ubovu mifupani mwake. Mawazo ya waongofu huyataka yanyokayo, lakini mashauri yao wasiomcha Mungu hutaka kudanganya tu. Maneno yao wasiomcha Mungu huotea damu za watu, lakini vinywa vyao wanyokao huwaponya. Wasiomcha Mungu wanapofudikizwa hawako tena, lakini nyumba za waongofu husimama. Mtu husifiwa, kama akili zake zilivyo, lakini mwenye moyo mpotovu hubezwa. Kunyenyekea na kujitumikia mwenyewe ni kwema, kuliko kujitukuza na kukosa vilaji. Mwongofu huzijua roho za nyama wake, afugao lakini huruma zao wasiomcha Mungu ni ukali tu. Alilimiaye shamba lake hushiba vilaji, lakini akimbiliaye mambo yaliyo ya bure amepotelewa na akili. Asiyemcha Mungu hutamani mateka ya wabaya, lakini mashina ya waongofu huchipuka. Mapotovu ya midomo ni kama tanzi baya, lakini mwongofu huponyoka akisongwa. Kila mtu hushiba vema mazao ya kinywa chake, mikono ya mtu iliyoyafanya, humrudia mwenyewe. Njia ya mjinga hunyoka machoni pake, lakini mwerevu wa kweli husikia shauri la mwingine. Mjinga hujulikana kwa kukasirika papo hapo, lakini aerevukaye huziba masikio akitukanwa. Asemaye yaliyo kweli hutangaza yaongokayo, lakini shahidi ya uwongo hudanganya. Wako wapuzi wachomao mioyo ya watu kama upanga, lakini ndimi zao walio werevu wa kweli huponya. Midomo yenye kweli hukaa kale na kale, lakini ndimi za uwongo hukaa kitambo kidogo tu. Udanganyifu umo mioyoni mwao watungao mabaya, lakini wenye mshauri ya utengemano hufurahisha. Mwongofu hapatwi na mapotovu yo yote, lakini wasiomcha Mungu hujaa mabaya. Midomo ya uwongo humtapisha Bwana, lakini wafanyao yaliyo kweli humpendeza. Mtu aerevukaye huyaficha, anayoyajua, lakini mioyo ya wapumbavu huutangaza ujinga. Mikono yao wajihimizao kufanya kazi hupata ufundi, lakini mikono ilegeayo hujipatia utumwa. Majonzi yaliyomo ndani ya moyo wa mtu huulemeza, lakini neno jema huufurahisha. Mwongofu humwongoza mwenzake, lakini njia zao wasiomcha Mungu huwapoteza. Mwenye uvivu hamkimbizi nyama wake wa kuwinda, lakini mali za mtu zilizo na kima ni kujihimiza kufanya kazi. Katika njia ya wongofu ndipo, uzima ulipo; njia hiyo inapopitia, kifo hakipo hapo. Mwana mwerevu wa kweli hutaka kuonywa na baba, lakini mfyozaji hasikii akikemewa. Kila mtu hula mema, kinywa chake kilichoyazaa, lakini roho zao wavunja maagano hula makorofi. Akilindaye kinywa chake huilinda roho yake, lakini aifunuaye midomo yake hujiangamiza. Roho yake mvivu hutamani vingi pasipo kupata kitu, lakini roho zao wajihimizao kufanya kazi hushibishwa sana. Mwongofu huchukia neno la uwongo, lakini asiyemcha Mungu hufanya yachukizayo nayo yatwezayo. Mwongofu humlinda ashikaye njia isiyokosesha, lakini kuacha kumcha Mungu humwangusha mkosaji. Wako wanaojitendekeza kuwa wenye mali, lakini hawana kitu, tena wako wanaojitendekeza kuwa maskini, lakini wana mali nyingi. Makombozi ya roho ya mtu ni mali zake nyingi, lakini maskini hasikii makemeo yo yote. Mwanga wa waongofu huangaza kwa furaha, lakini taa zao wasiomcha Mungu huzimika. Hakuna mengine, majivuno yanayoyaleta, ila ugomvi tu, lakini kwao wanaotaka mashauri mema uko werevu wa kweli. Mali zilizopatikana bure tu hupunguka upesi, lakini azikusanyaye kwa kazi za mkono wake huziongeza. Uliyoyangojea yakikawia sana huuguza moyo, lakini kuyapata, uliyoyatamani, ni mtu wa uzima. Alibezaye Neno hupatiwa mwangamizo nalo, lakini aogopaye kulikosea agizo hupata malipo. Maonyo ya mwerevu wa kweli ni kisima cha uzima, maana ni kuepuka penye matanzi ya kifo. Ujuzi mwema huleta mapendeleo, lakini njia zao walioacha kumcha Mungu hushupaza. Mwerevu hufanya yote kwa ujuzi, lakini mpumbavu hujikuza kwa mapumbavu yake. Mjumbe asiyemcha Mungu huanguka kwa ubaya, lakini mtume mwelekevu huponya. Ukiwa na matusi humpata akataaye kuonyeka, lakini aangaliaye akikanywa hupata heshima. Kuyapata, mtu aliyoyatamani, huipendeza roho yake, lakini yanayowatapisha wapumbavu ni kuacha mabaya. Atembeaye na werevu wa kweli huerevuka kweli, lakini rafiki ya wapumbavu hupata mabaya. Mabaya huwakimbiza wakosaji, lakini waongofu Mungu huwalipa mema. Mwema huwaachia wanawe na wana wao mali zake, lakini mapato ya mkosaji hulimbikiwa mwongofu. Shamba, waliloanza kulilima, huwapatia wakiwa vilaji vingi, lakini wengine hupokonywa kwa kufanya yasiyo sawa. Amnyimaye mwanawe fimbo humchukia, lakini ampendaye hakawii kabisa kumchapa. Mwongofu hupata kula, hata aishibishe roho yake, lakini matumbo yao wasiomcha Mungu huona njaa. Werevu wa kweli wa wanawake huzijenga nyumba zao, lakini ujinga wao huzibomoa kwa mikono yao wenyewe. Ashikaye njia inyokayo humcha Bwana, lakini azipotoaye njia zake humbeza. Kinywani mwa mjinga imo fimbo ya majivuno, lakini midomo ya werevu wa kweli huwalinda. Pasipo ng'ombe zizi hukaa likiwa safi, lakini mapato huwa mengi, nguvu za ng'ombe zinapotumiwa. Shahidi mwenye kweli haongopi, asemaye maneno ya uwongo ni shahidi mwenye uwongo. Mfyozaji akitafuta werevu wa kweli haupati, lakini mtambuzi hupata upesi kujua maana. Toka kwa mtu aliye mjinga! Kwani kwake huoni midomo ijuayo maana. Werevu wa kweli wa mtu aerevukaye humtambulisha njia yake, lakini ujinga wa wapumbavu huwadanganya. Wajinga hufyoza wakikora manza, lakini wanyokao hupendezana. Moyo wenyewe hujua uchungu wa roho yake, hata katika furaha yake mwingine hajitii humo. Nyumba zao wasiomcha Mungu hubomolewa, lakini mahema yao wanyokao yatachanua. Ziko njia zinyokazo machoni pa watu, lakini mwisho wao huenda kufani. Hata ukicheka, moyo unaweza kuumia, mara nyingi mwisho wa furaha ni majonzi. Moyo ukirudi nyuma, mtu hushibishwa mapato ya njia zake, naye mtu mwema huyapata, aliyoyasumbukia. Mjinga huitikia maneno yote, lakini aerevukaye hupatambua, anapokwenda. Mwerevu wa kweli huogopa, huepuka penye mabaya, lakini mjinga huchafuka, kisha huwaza, ya kuwa mambo yametulia. Mwenye moyo mdogo hufanya yenye ujinga, naye mwenye mawazo mabaya huchukiwa. Wasiojua kitu hujipatia ujinga, uwe fungu lao, lakini waerevukao huvikwa vilemba vya ujuzi. Wabaya sharti wawainamie wema, nao wasiomcha Mungu sharti wasimame milangoni pao waongofu. Hata rafiki yake humchukia maskini, lakini wampendao mwenye mali ni wengi. Amwendeaye mwenziwe na kumbeza hukosa, lakini awahurumiaye wanyonge ni mwenye shangwe. Je? Wawazao mabaya hawapotei? Lakini wawazao mema hujipatia upendeleo wa kweli. Masumbuko yote yako na mapato, lakini yaliyo maneno matupu ya midomo huleta ukosefu tu. Kwao werevu wa kweli mali zao ni kama kilemba, lakini ujinga wa wapumbavu huwa ujinga. Shahidi mwenye kweli huponya roho za watu, lakini asemaye uwongo huziponza. Mtu akimcha Bwana analo egemeo lenye nguvu, nao wanawe wanapo pao pa kukimbilia. Kumcha Bwana ni kisima cha uzima, tena ni kuondoka penye matanzi ya kifo. Utukufu wa mfalme umo katika wingi wa watu, lakini watu wanapokwisha, mkuu wao huangamia. Mvumilivu anao utambuzi mwingi, lakini mwenye moyo mdogo hukuza ujinga. Moyo mpole ni uzima wa mwili, lakini wivu ni kama ugonjwa wa ubovu mifupani. Akorofishaye mnyonge humsimanga aliyemwumba, lakini amheshimuye humhurumia mkiwa. Kwa ubaya wake asiyemcha Mungu hukumbwa, aanguke, lakini mwongofu hata kufani yuko na kimbilio lake. Moyoni mwa mtambuzi ndimo, werevu wa kweli unamotua, lakini yaliyomo mioyoni mwa wapumbavu hujulikana. Wongofu hukuza taifa, lakini ukosaji hutweza makabila mazima. Mfalme hupendezwa na mtumishi mwenye akili, lakini humkasirikia sana anayemtweza. Jibu lenye upole hutuliza makali, lakini neno liumizalo hukasirisha sana. Ndimi zao walio werevu wa kweli husema ujuzi mwema, lakini vinywa vya wapumbavu hububujika ujinga. Macho ya Bwana huwa po pote, huwatazama wabaya na wema. Upole wa ulimi ni mti wa uzima, lakini udanganyifu uliomo huvunja moyo. Mjinga hukataa kuonywa na baba yake, lakini aangaliaye akikanywa huerevuka. Nyumbani mwa mwongofu mna limbiko kubwa, lakini mapato yake asiyemcha Mungu utawanyika. Midomo yao walio werevu wa kweli humwaga ujuzi, lakini mioyo ya wapumbavu haifanyi hivyo. Vipaji vya tambiko vyao wasiomcha humtapisha Bwana, lakini maombo yao wanyokao humpendeza. Njia yake asiyemcha humtapisha Bwana, lakini humpenda aukimbiliaye wongofu. Ayaachaye mapito yampasayo hupata mapigo mabaya, achukiaye kukanywa hufa. Kuzimu nako, wafu wanakopotelea, kuko mbele ya Bwana; tena je? Mioyo ya wana wa Adamu haitakuwa wazi zaidi? Mfyozaji hapendi, mtu akimkanya, wala haendi kwao werevu wa kweli. Moyo wenye furaha huuchangamsha uso, lakini moyo ukisikitika, roho hupondeka. Moyo wa mtambuzi hutafuta ujuzi, lakini vinywa vya wapumbavu hujilisha ujinga. Siku zote za mtu atesekaye ni mbaya, lakini moyo mwema hufanana na karamu ya siku zote. Machache yake amwogopaye Bwana ni mema kuliko malimbiko mengi yamhangaishayo mwenyewe. Kula maboga na mtu wa kupendana naye ni kwema kuliko ng'ombe ya manono, ukila na mtu wa kuchikzwa naye. Mtu mkali huzusha magomvi, lakini mvumilivu hutuliza mateto. Njia ya mvivu hufanana na boma lenye miiba mikali, lakini mapito yao wanyokao ni njia zilizotengenezwa. Mwana mwerevu wa kweli humfurahisha baba yake, lakini mtu mpumbavu humbeza mama yake. Ujinga humfurahisha aliyepotelewa na akili, lakini mwenye utambuzi huunyosha mwenendo wake. Nayo mawazo mema hayafanikiwi pasipo kupiga mashauri, lakini wenye kuongoza wanapokuwa wengi, huendelea. Mtu hufurahia jibu jema la kinywa chake, nalo neno lisemwalo panapopasa ni zuri zaidi. Njia yake aerevukaye ya kwenda uzimani huelekea juu, kusudi ajiepushe kuzimuni huko chini. Nyumba zao wenye majivuno Bwana huzibomoa, lakini mipaka ya wajane huishupaza. Mawazo ya wabaya humtapisha Bwana, lakini maneno yampendezayo ndiyo yatakatayo. Atakaye mapato ya upotovu huwavuruga waliomo nyumbani mwake, lakini achukiaye mapenyezo hujipatia uzima. Moyo wa mwongofu huyawaza, atakayoyajibu, lakini vinywa vyao wasiomcha Mungu hububujika mabaya. Bwana huwakalia mbali wasiomcha, lakini malalamiko ya waongofu huyasikia. Macho yakiangaza, moyo hufurahi, habari njema huishupaza mifupa. Sikio linalosikia maonyo yanayompatia mtu uzima hupenda kukaa kwao werevu wa kweli. Akataaye kuonywa huitupa roho yake, lakini asikiaye akikanywa hujipatia akili zaidi. Amchaye Bwana huonyeka, ajipatie werevu wa kweli, nayo macheo hutanguliwa na unyenyekevu. *Mtu huyatengeneza mambo ya moyo, lakini Bwana huyapa, ulimi unayoyajibu. Njia zote za mtu hutakata machoni pake, lakini Bwana huzijaribu roho. Mtupie Bwana yote utakayoyafanya! Ndivyo, mawazo yako yatakavyotimia. Bwana aliyaumba yote kulitimiza neno, alitakalo, hata yeye asiyemcha alimwumbia kuiona siku mbaya. Wote wajikuzao mioyoni mwao humtapisha Bwana, ingawa wapeane mikono, hawana budi hupatilizwa. Manza huondolewa kwa huruma na kwa welekevu, kwa kumcha Bwana mtu huepuka penye mabaya. Njia za mtu zikimpendeza Bwana, hupatanisha naye hata wachukivu wake. Machache yapatikanayo kwa wongofu ni mema kuliko mapato mengi yapatikanayo kwa njia zisizo sawa. Moyo wa mtu hujiwazia njia zake, lakini Bwana ndiye anayeiendesha miguu yake.* Midomo ya mfalme inayoyasema ni fumbo, kwa kukata shauri kinywa chake hakidanganyi. Mizani na vipimo vya kweli hujua Bwana, vijiwe vyote vya kupimia vilivyomo mifukoni ni kazi zake. Kufanya maovu hutapisha wafalme, kwani kiti cha kifalme hupata nguvu kwa wongofu. Midomo isemayo yaongokayo hupendeza wafalme, nao wasemao yanyokayo huwapenda. Makali ya mfalme hufanana na wajumbe wa kifo, lakini mtu mwerevu wa kweli huyatuliza. Uso wa mfalme ukiangaza hupatia watu uzima, akipendezwa hufanana na wingu lenye mvua ya masika. Kupata werevu wa kweli ni kwema kuliko kupata dhahabu, kupata utambuzi hufaa zaidi kukuchagua kuliko kupata fedha. Mwenendo wao wanyokao huepuka penye mabaya, aiangaliaye roho yake huilinda njia yake. Majivuno hufuatwa na kuanguka, nako kujikuza rohoni hufuatwa na kujikwaa. Kujinyenyekeza pamoja nao wanyonge ni kwema kuliko kugawanya mapokonyo pamoja nao wajivunao. Aliangaliaye Neno huona mema, naye amwegemeaye Bwana ni mwenye shangwe. Mwenye moyo uerevukao kweli huitwa mtambuzi, midomo isemayo maneno matamu huendesha mafunzo. Kutumia akili humpatia mwenyewe kisima cha uzima, lakini mapigo ya wajinga huwapatia ujinga tu. Moyo wa mwerevu wa kweli hukifundisha kinywa chake, nayo midomo yake huendesha mafunzo. Maneno yapendezayo ni asali iliyo nzuri yenyewe, roho huyaona kuwa matamu, nayo mifupa hupata uzima mumo humo. Ziko njia zinyokazo machoni pa mtu, lakini mwisho hujulika kuwa njia za kwenda kufani. Roho ya msumbufu hujisumbukia, kwani kinywa chake humlemea. Mtu asiyefaa kitu huchimbua mabaya, nayo maneno ya midomo yake hufanana na moto uunguzao. Mtu mpotovu huzusha magomvi, msingiziaji hutenganisha watu waliopendana. Mtu mkorofi humpoteza mwenziwe akimwongoza katika njia isiyo njema. Ayafumbaye macho yake huwaza mapotovu, akazaye kuifunga madomo yake amikwisha kutunga mabaya. Mvi ni kilemba chenye utukufu, huonekana katika njia ya wongofu. Uvumilivu ni mwema kuliko ufundi wa vita, ajitawalaye moyoni mwake ni mwema kuliko atekaye miji. Kura hupigwa katika mikunjo ya nguo, lakini mashuri yote hukatwa na Bwana. Kula kitonge kikavu cha wali na kutulia ni kwema, kuliko karamu za nyumbani mlimo na magomvi tele. Mtumishi mwenye akili humshinda mwana wa bwana wake atwezaye, hugawanya mali zilizoachawa na Bwana pamoja na ndugu zake yule. Chungu cha kuyeyushia hujaribu fedha, nayo tanuru hujaribu dhahabu, lakini aijaribuye mioyo ni Bwana. Mtenda mabaya husikiliza midomo isemayo mapotovu, mwongo naye hutega sikio penye ulimi usemao mateto. Afyozaye maskini humsimanga aliyemwumba, afurahiaye mwangamizo hana budi hupatilizwa. Kilemba cha wazee ni wana wa wana wao, nao utukufu wa wana ndio wazazi wao. Mjinga hapaswi na maneno mazuri, sembuse mkuu na maneno ya uwongo! Matunzo ni kama kito kipendezacho machoni pake ayatoaye, po pote anapojielekeza hufanikiwa. Afunikaye makosa hutafuta kupendwa, lakini azushaye mambo ya kale hutenganisha rafiki waliopendana. Mtambuzi akikanywa husikia zaidi kuliko mpumbavu akipigwa fimbo mia. Mbaya anayoyatafuta ni ukatavu tu, kwa hiyo kwake hutumwa mjumbe mshupavu. Kukutana na chui mke aliyenyang'anywa watoto ni kwema kuliko kukutana na mpumbavu aufuataye ujinga wake. Mtu aliyepata mema akiyalipa kwa kufanya mabaya, basi, nyumbani mwake yeye mabaya hayakomeki. Kuzua magomvi ni kufungua maji, yajiendee tu; kwa hiyo acha magomvi ukiwa hujakenua meno bado. Kumkania akosaye na kumsingizia asiyekosa, kote kuwili humtapisha Bwana. Je? Fedha mkononi mwa mpumbavu ni za nini? Za kununua werevu wa kweli? Tena akili haziko! Rafiki hupenda siku zote, naye huzaliwa penye masongano, awe ndugu kweli. Mtu aliyepotelewa na akili ni yule anayepeana mkono na mwingine, anayejitoa kwa mwingine kuwa dhamana ya mwenziwe. Apendaye ugomvi hupenda kupotoa, aukuzaye mlango wake hutafuta mbomoko. Mwenye moyo mdanganyifu hapati mema, naye mwenye ulimi wa upotovu huangushwa na mabaya. Azaaye mpumbavu hujipatia majonzi, hata babake mjinga hapati furaha. Moyo wenye furaha husaidia vema kupona magonjwa, lakini roho ipondekayo hukausha kiini cha mifupa. Asiyemcha Mungu huchukua mapenyezo na kuyaficha kifuani, ayapotoe mashauri, yasifuate njia zilizo sawa. Machoni pake mtambuzi upo werevu wa kweli, lakini macho ya mpumbavu hutembea mapeoni kwa nchi. Mwana mpumbavu humsikitisha baba yake, naye mama yake aliyemzaa humpatia machungu. Mtu asiyekosa haifai humtoza fedha, wala hupiga wakuu kwa ajili ya unyofu wao. Ayazuiaye maneno yake ni mwenye ujuzi wa kweli, naye aitulizaye roho yake ni mtu mtambuzi. Naye mjinga akinyamaza huwaziwa kuwa mwerevu wa kweli, aifumbaye midomo yake ni mtambuzi. Ajitengaye na watu hutaka kuyafanya, ayatamaniyo hukataa kwa ukali yote yafaayo. Mpumbavu hapendezwi na utambuzi, hutaka tu kuyafanya yaliyomo moyoni mwake. Asiyemcha Mungu anapofika, nayo mabezo hupafika, tena nayo matusi huja pamoja na matwezo. Maneno ya kinywa cha mtu aliye mtu kweli ni maji yenye vilindi, ni kijito kitoacho maji mengi, ni kisima cha werevu wa kweli. Haifai huutazama uso wa mtu aliyekosa na kumpotoa shaurini asiyekosa. Midomo ya mpumbavu huleta ugomvi, nacho kinywa chake huita mapigo. Kinywa cha mpumbavu humwangamiza, nayo midomo yake ni tanzi liinasalo roho yake. Maneno ya msingiziaji ni matamu kama vyakula vya urembo navyo hushuka tumboni ndani. Ailegezaye mikono katika kazi ni ndugu yake azitawanyaye mali zake. Jina la Bwana ni mnara wenye nguvu; ndipo, mwongofu anapokimbilia, akapona. Mali za mkwasi ni ngome yake yenye nguvu, katika mawazo yake ni boma liendalo juu sana. Moyo wa mtu ukijivuna, nyuma huvunjwa, nayo macheo hutanguliwa na unyenyekevu. Kama mtu anajibu akiwa hajasikia bado, ni ujinga, nao humpatia soni. Roho ya kiume huyavumilia magonjwa yake, lakini roho ikipondeka, yuko nani awezaye kuyavumilia? Moyo wa mtambuzi hujipatia ujuzi, nayo masikio ya walio werevu wa kweli hutafuta ujuzi. Vipaji vya mtu humpanulia njia, tena humfikisha kwa wakuu. Atokeaye wa kwanza hushinda shaurini, mwenziwe anapotokea humwumbua. Kura hukomesha magomvi, huwatenganisha nao wenye nguvu. Ndugu apotolewaye hushupaa kuliko mji ulio na boma lenye nguvu, nayo magomvi yaliyo hivyo hufanana na makomeo ya jumba kubwa. Kila mtu hulishibisha tumbo lake mazao ya kinywa chake, kweli hushiba mazao ya midomo yake. Kufa na uzima hushikwa na ulimi, autunzaye na kuupenda hula mazao yake. Aliyepata mkewe amepata kipaji chema, akijipatia kwa Bwana yampendezayo. Maskini husema na kulalamika, lakini mwenye mali humjibu na kumtolea nguvu. Mwenye rafiki wengi huangamia mara nyingi, lakini yuko rafiki anayeambatana na mtu kuliko ndugu. Mkiwa aishikaye njia yake pasipo kukosa na mwema kuliko mpotovu wa midomo aliye mpumbavu. Roho ikosayo ujuzi siyo njema, naye mwenye haraka ya kupiga mbio kwa miguu hukosa. Ujinga wa mtu huipotoa njia yake mwenyewe, lakini moyo wake humkasirikia Bwana. Kuwa na mali huongeza rafiki, wawe wengi, lakini mnyonge huachwa na rafiki zake. Shahidi ya uwongo hana budi kupatilizwa, asemaye na kuongopa haponi. Watu wengi hulalamika usoni pa wakuu, watu wote huwa rafiki zake awapaye matunzo. Maskini huchukiwa na ndugu zake wote, wanaozidi ni rafiki zake, hutengana naye humwacha mbali; akiwafuata, aseme nao, sio rafiki zake tena. Apataye akili hujipenda mwenyewe utambuzi huona mema. Shahidi ya uwongo hana budi kupatilizwa, asemaye na kuongopa huangamia. Mpumbavu hapaswi na kutumia yenye urembo, sembuse mtumishi, hapaswi na kuwatawala wafalme. Akili za mtu humvumilisha, utukufu wake umo katika kuwaondolea wengine mapotovu yao. Ukali wa mfalme ni kama ngurumo ya simba, lakini upole wake ni kama umande unyweshao majani. Mwana mpumbavu humpatia baba yake mabaya, lakini magomvi ya mwanamke huwa mchirizi usiokoma kuchuruzika. Nyumba na mali watu huachiwa na baba zao, lakini mwanamke mwenye akili hutoka kwa Bwana. Uvivu humpatia mtu usingizi mwingi, nayo roho ya mtu afanyaye kazi na kulegeza mikono huona njaa. Aliangaliaye agizo la Mungu hujiangalia mwenyewe, lakini azibezaye njia zake hufa. Ahurumiaye mnyonge humkopesha Bwana, ndiye atakayemlipa tendo lake. Mpige mwanao unapoweza kumngojea, aonyeke, lakini usiwaze moyoni mwako kumwua! Mwenye makali mengi hutozwa malipo, kwani ukimwacha tu, unayazidisha makali yake. Yasikie mashauri, unayopewa, uonyeke, kusudi uerevuke kweli katika siku zako zijazo. Moyoni mwa mtu yamo mawazo mengi, lakini shauri la Bwana ndilo litakalokuwa. Ugawiaji wa mtu hutokea katika mapenzi yake, naye maskini ni mwema kuliko mwenye uwongo. Kumcha Bwana hupeleka uzimani, hivyo mtu hulala na kushiba pasipo kupatwa na mabaya. Mvivu akiutia mkono wake katika bakuli haurudishi kinywani mwake. Ukimpiga mfyozaji, ndipo, mjinga atakapoerevuka, ukimwonya mtambuzi, ndipo, atakapotambua ujuzi. Amtesaye baba yake na kumfukuza mama yake ni mwana atiaye soni kwa kutweza. Mwanangu, acha kuyasikiliza mafunzo, ukitaka kuyakosea tena maneno ya ujuzi! Shahidi asiyefaa kitu hufyoza mashauri yaliyo sawa, navyo vinywa vyao wasiomcha Mungu hujilisha mapotovu. Mashauri ya wafyozaji yamekwisha kutengenezwa, nayo mapigo ya migongoni kwa wapumbavu yako tayari. Mvinyo ni mfyozaji, nacho kileo huleta makelele, kila atokaye hapo na kupepesuka hakuerevuka. Tisho la mfalme ni ngurumo ya simba, amkasirishaye hujikosea mwenyewe. Mtu ajitengaye penye ugomvi huheshimiwa, lakini kila mjinga hukenua meno. Mvivu hataki kulima tangu hapo, kipupwe kinapoanza, tena akitafuta vilaji mavunoni, haviko. Maji yenye lindi ni mashauri yaliyomo noyoni mwa mtu, lakini mtu mtambuzi hujua kuyateka. Watu wengi hutangaza, ila mtu akizikuza huruma zake yeye, lakini aonaye mtu mwenye welekevu wa kweli yuko nani? Aishikaye njia yake pasipo kukosa ni mwongofu, wanawe wamfuatao nyuma ndio wenye shangwe. Mfalme akaaye katika kiti chake cha kukatia mashauri huyatawanya kwa macho yake mabaya yote. Yuko nani awezaye kusema: Nimeung'aza moyo wangu? Nimetakata, makosa yangu yamekwisha kuondoka? Vipimo vya namna mbili na pishi za namna mbili, zote mbili humtapisha Bwana. Hata kijana hujulika kwa matendo yake, kama kazi zake zinatakata, kama zinakwenda sawa. Sikio lisikialo na jicho lionalo, Bwana ndiye ayatengenezaye yote mawili. Usiupende usingizi, usije kuwa mkosefu! Yafumbue macho yako! Ndipo, utakaposhiba chakula. Mnunuzi husema: Ni kibaya, ni kibaya, lakini akiisha kwenda zake hujichekea. Ingawa dhahabu ni lulu ziwe nyingi, lakini kiko kitu kizipitacho, ndio midomo yenye ujuzi. Zichukue nguo zake yeye aliyejitoa kuwa dhamana ya mwingine, kwa ajili yao walio wageni mnyang'anye yeye mali zake. Vilaji vilivyopatwa kwa udanganyifu mtu huviona kuwa vitamu, lakini mwisho kinywa chake hujaa vijiwe vya changarawe. Mawazo yaliyopigiwa mashauri mema hufanikiwa, ukipiga vita vipige na kuzitumia akili! Atembeaye na kusingizia hufunua mashauri ya njama, naye afumbuaye midomo usifanye bia naye. Amwapizaye baba yake na mama yake, taa yake huzimika katika giza lizidishalo. Ukianza kujipatia fungu la mali kwa kupokonya upesiupesi, mwisho hazibarikiwi. Usiseme: Na nilipishe mabaya! Ila mngojee Bwana! Ndiye atakayekusaidia. Vipimo viwili humtapisha Bwana, nayo mizani ya kudanganyia haifai. Bwana ndiye anayeiendesha miguu ya mtu, maana mtu anawezaje kuitambua njia yake? Mtu hujinasa kwa kujisemea tu: Hii mali ya Bwana, na kuyafikiri halafu, aliyoyaapa. Mfalme mwerevu wa kweli huwapepeta wasiomcha Mungu, akipitisha juu yao gari la kupuria. Roho ya mtu ni taa, aliyopewa na Bwana, nayo huyachunguza yote yaliyomo tumboni. Upole na welekevu humlinda mfalme, naye hukishikiza kiti chake cha kifalme kwa upole. Utukufu wa vijana ni nguvu zao, nao urembo wa wazee ni mvi. Mavilio yenye vidonda humtakasa mtu, mabaya yamtoke, ijapo mapigo yaingie mpaka tumboni ndani. Moyo wa mfalme ni kama vijito vya maji mkononi mwa Bwana, humpeleka pote panapompendeza. Njia zote za mtu hunyoka machoni pake, lakini Bwana huijaribu mioyo. Kufanya wongofu na kupiga mashauri yaliyo sawa humpendeza Bwana kuliko kutoa vipaji vya tambiko. Macho yajivunayo na moyo ujitutumuao ndio taa zao wasiomcha Mungu, nazo hukosesha. Mawazo yake ajikazaye kufanya kazi humpatia mengi, lakini mwenye haraka hujipatia ukosefu tu. Kujipatia malimbiko kwa ulimi uongopao ni kama pumzi ipoteleayo angani tu, wayatakao hujitafutia kufa. Uangamizi wao wasiomcha Mungu huwapokonya, kwa kuwa hukataa kufanya yaliyo sawa. Njia ya mtu akoraye manza hupotoka sana, lakini matendo yake anyokaye hutakata. Kukaa darini pembeni ni kwema kuliko kukaa na mwanamke mgomvi katika nyumba moja. Roho yake asiyemcha Mungu hutamani mabaya, mwenziwe hapati huruma machoni pake. Mfyozaji akitozwa fedha, mjinga huerevuka, naye mwerevu wa kweli akifundishwa hupata ujuzi zaidi. Yuko mwongofu aiangaliaye nyumba yake asiyemcha Mungu, naye huwapotoa wasiomcha Mungu, wapatwe na mabaya. Alizibaye sikio lake, lisisikie kilio cha mnyonge, naye atakapolia hatajibiwa. Kipaji kipenyezwacho hutuliza ukali, nayo matunzo yafichwayo penye kujua huzima nao moto mkali. Furaha ya mwongofu ni kufanya yaliyo sawa, lakini wafanyao mapotovu hukuwazia kuwa mwangamizo. Mtu apoteaye kwa kuiacha njia ya ujuzi hupata kupumzika katika mkutano wao waliokufa. Apendaye michezochezo huwa mtu akosaye vyote, apendaye mvinyo na vinono hatapata mali. Asiyemcha Mungu hana budi kumkomboa mwongofu, naye avunjaye agano hulipa mahali pao wanyokao. Kukaa katika nchi ya nyika ni kwema kuliko kukaa na mwanamke mgomvi mwenye matata. Limbiko lipendezalo na mafuta yamo katika makao ya werevu wa kweli, lakini mtu mjinga huyameza. Afanyaye bidii kuufuata wongofu na upole hupata uzima na wongofu na utukufu. Mwongofu hupanda na kuuingia mji wa wenye nguvu, nalo boma lao gumu, walilolitegemea, huliangusha. Akiangaliaye kinywa chake na ulimi wake hujiangalia mwenyewe, asisongwe na maneno. Mtu ajitutumuaye kwa majivuno, aitwaye mfyozaji hufanya mambo, anayofundishwa na majivuno yake yafurikayo. Tamaa za mvivu humwua, kwa kuwa mikono yake hukataa kufanya kazi. Kila siku yako yanayotamaniwa kwa tamaa, lakini mwongofu hutoa mali, hawanyimi wamwombao. Wasiomcha Mungu wakitoa vipaji vya tambiko humtapisha, zaidi wakivitoa na kuyaficha mawazo yao mabaya. Shahidi ya uwongo huangamia, lakini mtu asikiaye kwanza atasema siku zote. Mtu asiyemcha Mungu huushupaza uso wake, lakini yeye anyokaye huishupaza njia yake. Hakuna werevu wa kweli, wala utambuzi, wala shauri njema mbele ya Bwana. Farasi huwekwa kuwa tayari siku za mapigano, lakini wokovu hutoka kwa Bwana. Sifa njema ina kima kuliko mali nyingi, upendeleo nao hufaa kuliko fedha na dhahabu. Mkwasi na maskini hukutana, aliyewaumba wote wawili ni Bwana. Mwerevu akiona mabaya hujificha, lakini wajinga hupita tu, wakapatwa nayo. Mapato ya unyenyekevu na ya kumcha Bwana ni mali na macheo na uzima. Miiba na matanzi yamo katika njia ya mpotovu, ajiangaliaye hujiepusha hapo. Mfundishe mtoto, apate kuijua njia yake, asiiache, hata atakapokuwa mzee. Mkwasi huwatawala maskini, naye akopaye ni mtumishi wake amkopeshaye. Apandaye uovu huvuna mapotovu, nayo fimbo iliyomtia ukali itakomeshwa. Atazamaye wengine kwa jicho lenye utu hubarikiwa, kwani humgawia mnyonge chakula chake. Mfukuze mfyozaji! Ndipo, ugomvi nao utakapotoka, ndipo, mteto nayo matusi yatakapokoma. Apendaye, moyo utakate, naye mwenye midomo ipendezayo huwa rafiki yake mfalme. Macho ya Bwana humlinda mwenye ujuzi, lakini maneno yake avunjaye agano huyapindua. Mvivu husema: Simba yuko nje, nitauawa peupe barabarani. Vinywa vya wanawake wa wengine ni mashimo marefu, Bwana anayemchukia, utumbukia humo. Ujinga umefungiwa moyoni mwa mtoto, lakini fimbo ya kumchapa itautoa mwake. Amkorofishaye mnyonge humpatia mali nyingi, amgawiaye mwenye mali humpunguzia mali zake. Litege sikio lako, uyasikilize maneno ya werevu wa kweli! Nao moyo wako uuelekezee ujuzi wangu! Kwani ni mazuri ya kuyaangalia mwako ndani, yote pamoja yawe tayari kutumiwa na midomo yako. Kwa kwamba: Bwana na awe kimbilio lako, kwa hiyo ninakufundisha leo wewe mwenyewe. Je? Sikukuandikia mambo makuu, yakupe mashauri mema ya kukujulisha maana? Ndiyo yatakayokujulisha maongozi ya kweli na maneno ya kweli, upate kuwajibu maneno ya kweli wao waliokutuma. Usimnyang'anye mnyonge! Kwani ni mnyonge, wala mwenye mateso usimkanyage mlangoni! Kwani Bwana huwagombea, wakigombezwa na watu, nao wanaowapokonya huwapokonya roho zao. Usifanye bia na mtu mwenye moyo mdogo, wala usitembee na mtu mwenye makali kama ya moto, kusudi usijizoeze mwenendo wake, ukajipatia tanzi la roho yako. Usiwe nao wanaopeana mikono wakijitoa kuwa dhamana za wengine kwa ajili ya madeni yao! Usipoweza kulipa halafu, mbona wakichukue kitanda chako, unachokilalia? Usisogeze mawe ya mipaka ya kale, baba zako walioyayaweka! Ukiona mtu ajihimizaye kazi zake, atakwenda kutumikia wafalme, asitumikie watu walio watuwatu tu. Ukikaa chakulani kwa mtawalaji sharti umtambue yeye aliopo usoni pako. Jibandikie kisu kooni pako wewe ukiwa mwenye tamaa ya kula sana! Usivitamani vilaji vya urembo vya mwingine! Kwani ni vyakula vya udanganyifu. Usijisumbue kupata mali nyingi, ukaacha kuutumia utambuzi wako kwa ajili ya hizo mali! Au sivyo? Ukizitupia macho yako, basi, haziko tena, nazo hujitengenezea mabawa kama ya tai ya kurukia kwenda mbinguni. Usile chakula chake mwenye jicho baya, wala usivitamani vyakula vyake vya urembo! Kwani yeye ni kama mtu ahesabuye yote rohoni mwake; hukuambia: Haya! Ule, unywe! lakini moyo wake hauko kwako. Kwa hiyo utakitapika kitonge, ulichokila, nayo maneno yako yapendezayo yatakuwa umeyasema bure tu. Usiseme masikioni pa mpumbavu! Kwani atayabeza maneno yako, uliyoyasema kwa akili. Usisogeze mawe ya mipaka ya kale, wala usiingie mashambani kwao waliofiwa na wazazi wao! Kwani mkombozi wao ni mwenye nguvu, yeye huwagombea, wakigombezwa na wewe. Ushurutishe moyo wako, uonyeke, nayo maskio yako, yasikie maneno ya ujuzi! Usimnyime mtoto mapigo! ukimpiga kwa fimbo, hatakufa. Wewe ukimpiga kwa fimbo utaiokoa roho yake kuzimuni. Mwanangu, moyo wako ukierevuka kweli, moyo wangu mimi utafurahi nao. Maini yangu yatashangilia, midomo yako ikisema yanyokayo. Moyo wako usione wivu kwa ajili ya wakosaji, ila kaa tu na kumcha Bwana siku zote! Kwani yote yako na mwisho wao, lakini kingojeo chako hakitaangamia. Wewe mwanangu, sikiliza, uereuke kweli, kauongoze moyo wako katika njia hii! Usiwe mwenzao wanywaji wa mvinyo, wala wao walao nyama kwa ulafi! Kwani mnywaji na mlafi watachukuliwa mali zao, kwani usingizi mwingi huvika watu vitambaa vichakavu. Msikie baba yako aliyekuzaa! Usimbeze mama yako, akiwa mzee! Inunue kweli! Lakini usiiuze tena! Hata werevu wa kweli na usikivu na utambuzi! Babake mwana mwongofu hupiga shangwe nyingi, aliyezaa mwana mwerevu wa kweli humfurahia. Naye baba yako na mama yako na wakufurahie hivyo, yeye aliyekuzaa na apige shangwe! Mwanangu, nipe moyo wako, njia zangu ziyapendeze macho yako! Kwani mwanamke mgoni ni shimo refu sana, naye aliye mwanamke wa mwingine ni kisima chembamba. Naye huotea kama mpokonyi, awaongoze kuwa wengi, wao wavunjao maagano kwa watu. Ni nani aliaye? Ni nani apigaye kite? Ni nani apatwaye na magomvi? Ni nani aombolezaye? Ni nani ajiumizaye bure? Ni nani aliye na macho mekundu? Ndio wao wanaokunywa mvinyo usiku kucha, ndio wao watembeao kutafuta vileo vikali. Usiitazame mvinyo, jinsi wekundu wake unavyopendeza, jinsi inavyometuka katika bilauri, inavyozidi utamu, ukiinywa! Mwisho huuma kama nyoka, huchoma kama pili; ndipo, macho yako yatakapoona mambo mageni, nao moyo wako utakaposema mapotovu; nawe utakuwa kama mtu alalaye chini baharini, au kama mtu alalaye pembeni juu ya mlingoti; utasema: Walinipiga, lakini sikuumia, walinichapa, lakini sikusikia. Nitaamka lini? Ndipo, nitakapokwenda kuitafuta tena. Usione wivu kwa ajili ya watu wabaya, wala usitamani kuwa mwenzao! Kwani mioyo yao huwaza mwangamizo, nayo midomo yao husema makorofi. Nyumba hujengwa kwa werevu wa kweli ikishikizwa kwa utambuzi. Kwa ujuzi vyumba vyake hujazwa vitu vyote vyenye kima vipendezavyo. Mtu mwerevu wa kweli ni mwenye nguvu, naye mwenye ujuzi huzidisha uwezo. Kwani kwa kuzitumia akili utapiga vita, wokovu nao huja kwa kupiga mashauri yaliyo mema. Werevu wa kweli humkalia mjinga juu sana, asiufikie, hakifunui kinywa chake mlangoni penye mashauri. Awazaye kufanyia wengine mabaya tu huitwa mtunga maovu. Mawazo ya mjinga ni ya ukosaji, naye mfyozaji huwatapisha watu. Ukilegea siku ya kusongwa, nguvu zako ni chache. Waponye wanaopelekwa kuuawa, nao wanokumbwakumbwa kwenda kuchinjwa sharti uwaopoe! Ukisema: Hatukuyajua, je? Yeye aijaribuye mioyo haitambui? Je? Yeye ailindaye roho yako haijui? Naye ndiye atakayemlipisha kila mtu matendo yake. Mwanangu, ule asali, kwani ni njema, ile asali iliyo safi yenyewe, kwani ni tamu, ukiitia kinywani. *Nao werevu wa kweli uujue, ya kuwa ni utamu wa roho; ukiupata, basi, mwisho utafanikiwa, nacho kingojeo chako hakitang'oleka. Wewe usiyemcha Mungu, usiotee penye kao la mwongofu, wala usipabomoe pake pa kulalia! Kwani mwongofu akianguka mara saba huinuka, lakini wasiomcha Mungu hujikwaza penye mabaya. Mchukivu wako akianguka, usifurahi, wala moyo wako usipige shangwe, akijikwaa. Bwana asivione, maana ni vibaya machoni pake, akaacha kumtolea yule makali yake. Usijichafushe moyo kwa ajili yao watendao mabaya wala usiwaonee wivu wasiomcha Mungu! Kwani mwisho wake mbaya hautakuwa mwema, nazo taa zao wasiomcha Mungu huzimika.* Mwanangu, mwogope Bwana, hata mfalme! Usifanye bia nao wanaoigeuzageuza mioyo! Kwani mara utatokea mwangamizo wao, tena yuko nani ajuaye, mabaya yatakapowapata nyote wawili? Mifano hii nayo ilitoka kwa watu werevu wa kweli. Upendeleo haufai kabisa shaurini. Amwambiaye mkosaji: Hukukosa, ndiye, makabila ya watu watakayemwapiza, koo zote watamtakia mabaya. Lakini wao wanaomchapa hupendeza, mbaraka ya kuwapatia mema huwajia. Kama mwenye kunonea midomo ya mwingine alivyo, ndivyo, alivyo mtu ajibuye maneno yaliyo sawa. Fanya kazi zako za huko nje, kajitengenezee mashamba yako, kisha jijengee nyumba yako! Usiwe shahidi ya kumshinda mwenzio bure! Je? Huko hutadanganya kwa midomo yako? Usiseme: Kama alivyonitendea mimi, ndivyo, nitakavyomtendea naye, nitamlipisha kila mtu matendo yake. Nilipopita penye shamba la mvivu napo penye mizabibu ya mtu aliyepotelewa na akili, nikapaona, pote palikuwa miiba tu, pote palikuwa pamefunikwa na viwawi, nacho kitalu chake cha mawe kilikuwa kimebomoka. Nilipoyaona nikayashika na kuyaweka moyoni mwangu mimi, niyatumie ya kunionya. Ukitaka kulala bado kidogo na kupumzika bado kidogo na kukunja mikono kitandani bado kidogo, kisha umaskini wako utakujia na kupiga mbio pamoja na ukosefu ulio kama mtu aliyevaa mata. Hii nayo ni mifano ya Salomo, waliyoikusanya watu wa Hizikia, mfalme wa Yuda. Utukufu wake Mungu ni kufunika jambo, utukufu wao wafalme ni kufunua jambo. Kama mbingu zilivyoko juu, kama nchi ilivyoko nako kuzimuni, ndivyo, mioyo ya wafalme inavyotushinda, isichunguzike. Mtu akiondoa mitapo katika fedha hutengeneza chombo kinachomfaa mwenye kuyeyusha. Mtu akimwondoa asiyemcha Mungu machoni pake mfalme, kiti chake cha kifalme hupata nguvu kwa wongofu. Usijitukuze mbele ya mfalme, wala usisimame mahali, wakuu walipo! Kwani kuambiwa: Sogea hapa mbele! ni kwema kuliko kunyenyekezwa penye macho ya mkuu yaliyokutazama. Usitokee upesi kugombana na mtu! Kwani mwisho utafanya nini, mwenzio akikutia soni? Kama yako ya kupigania na mwenzio, yapiganie! Lakini usifunue shauri la njama ya mwingine, mtu aisikiaye asikuapize, uchongezi wako ukakurudia. Kama machunguwa yaliyomo katika vyano vya fedha yalivyo, ndivyo, lilivyo neno linalosemwa papasapo. Kama pete ya dhahabu na mkufu wa dhahabu tupu wa shingoni ni maonyo ya mwerevu wa kweli yakiingia katika sikio lisikialo. Kama baridi ya theluji inavyofurahisha siku ya mavuno, ndivyo, mjumbe mwelekevu anavyowafurahisha waliomtuma kwani huzituliza roho za mabwana zake. Mawingu na upepo pasipo mvua ni mtu ajivuniaye vipaji vya uwongo, asivyovitoa. Kwa uvumilivu hushindwa naye mwamuzi nao ulimi mwororo huvunja mifupa. Kama umeona asali, ule na kuipima, usije kuitapika, kama ulijishibisha sana! Kawilia kuingia nyumbani mwa mwenzio, usije kumchokesha, akakuchukia. Nyundo ipondayo na upanga na mshale mkali ni mtu amshuhudiaye mwenziwe ushahidi wa uwongo. Jino livunjikalo na mguu utegukao ni kumwegemea mtu avunjaye maagano siku ya masongano. Avuaye nguo siku ya baridi, au siki itiwayo katika magadi ni mtu amwimbiaye mwenziwe nyimbo, moyo wake ukiwa mzito. Mchukivu wako akiwa ana njaa, mpe chakula! Akiwa ana kiu, mpe cha kunywa! Kwani hivyo utampalia makaa ya moto kichwani pake, naye Bwana atakulipa hayo. Upepo wa kaskazini huleta mvua, nao ulimi usingiziao hukasirisha nyuso. Kukaa darini pembeni ni kwema kuliko kukaa na mwanamke mgomvi katika nyumba moja. Kama maji ya baridi, roho iyatweteayo, ni habari njema itokayo katika nchi ya mbali. Kama chemchemi ivurugikavyo au kama kisima kiharibikacho ni mwongofu atukutikaye machoni pake asiyemcha Mungu. Kula asali nyingi hakufai, lakini kuyachunguza mambo mazito huleta macheo. Kama mji uliobomolewa kwa kukosa ukuta wa boma ulivyo, ndivyo, alivyo mtu asiyejua kuiangalia roho yake. Kama theluji isivyopatana na kiangazi, kama mvua isivyopatana na mavuno, ndivyo, macheo yasivyopatana na mpumbavu. Kama ndege anavyojiendea tu, kama kinega anavyoruka, ndivyo, kiapizo cha bure kilivyo, hakimfikii aapizwaye. Mjeledi humpasa farasi, nayo hatamu humpasa punda; ndivyo, fimbo inavyoipasa migongo ya wapumbavu. Usimjibu mpumbavu na kuufuata ujinga wake, usije nawe mwenyewe kufanana naye! Tena umjibu mpumbavu na kuufuata ujinga wake, asijiwazie mwenyewe kuwa mwerevu wa kweli! Mwenye kujikata miguu au mwenye kujinywesha makorofi ni mtu apelekaye habari kwa kutuma mpumbavu. Kama miguu ya kiwete isivyotumika, ndivyo, fumbo lilivyo kinywani mwa wapumbavu. Kama kutupa kifuko cha vito katika chungu ya mawe kulivyo, ndivyo, kumpa mpumbavu macheo kulivyo. Mwiba uliochoma mkono wa mlevi ni fumbo lililomo vinywani mwa wapumbavu. Fundi hutengeneza yote mwenyewe, lakini mpumbavu atafutaye watu wa mshahara huwapa kazi ya mshahara walio wapitaji tu. Kama mbwa anavyoyarudia matapiko yake, ndivyo, mpumbavu anavyoufanya ujinga wake mara ya pili. Kama unaona mtu aliye mwerevu wa kweli machoni pake mwenyewe, basi, mpumbavu hutegemeka kuliko huyo. Mvivu husema: Simba yuko njiani, kweli simba yuko barabarani katikati. Mlango hupinduka kwa bawaba zake, naye mvivu hujipindua kitandani pake. Mvivu akiutia mkono wake katika bakuli hushindwa kuurudisha kinywani mwake. Mvivu ni mwerevu wa kweli machoni pake kuliko watu saba wanaojua kujibu vizuri. Akamataye masikio ya mbwa apitaye ni mtu ajitiaye katika magomvi yasiyo yake. Kama mwenye wazimu alivyo atupaye mishale yenye moto ya kuua watu, ndivyo, alivyo mtu amdanganyaye mwenziwe, akasema: Je? Mimi sikumchekesha tu? Kwa kukosa kuni moto huzimika, vivyo kwa kukosa msingiziaji ugomvi hukoma. Makaa hufaa juu ya makaa yawakayo, nazo kuni hufaa motoni; ndivyo, mtu mgomvi anavyofaa kuchochea magomvi. Maneno ya msingiziaji ni kama vyakula vya urembo vinavyoshuka kuingia tumboni ndani. Kama fedha zenye mitapo zilizobandikwa juu ya kigae ni midomo isemayo maneno yapendezayo sana, moyo ukiwa mbaya. Kwa maneno ya modomo yake mchukivu hujificha, namo moyoni mwake umo udanganyifu, alioutia humo. Akisema maneno mazuri mno, usimtegemee! Kwani moyoni mwake yamo matapisho saba. Uchukivu hujificha katika ujanja, lakini shaurini ubaya wake huumbuliwa. Achimbaye mwina hutumbukia mwenyewe mle ndani, naye aporomoshaye jiwe hupondwa nalo. Ulimi wenye uwongo huwachukia, uliowaumiza, nacho kinywa kisemacho mororo huangamiza. Usijivunie siku ya kesho! Kwani huyajui, hiyo siku utakayoyazaa. Mwingine na akusifu, kisiwe kinywa chako! Mgeni akusifu, lakini isiwe midomo yako! Jiwe ni zito, nao mchanga ni mzigo, lakini masikitiko ya mpumbavu ni mazito kuliko yote mawili. Makali huwaka moto, nayo machafuko hufurikia, lakini awezaye kusimama penye wivu yuko nani? Kuonywa waziwazi ni kwema kuliko kupendwa na mtu avifichaye. Vidonda, anavyokutia mpenzi wako, vina maana ya kweli, lakini asiyekoma kukunonea ni mchukivu. Roho ya mtu ashibaye hubeza hata asali iliyo safi, lakini roho ya mtu aliye na njaa huona nayo machungu kuwa matamu. Kama ndege aliyekimbia tunduni mwake ndivyo, alivyo mtu aliyekimbia kwao. Mafuta na uvumba hufurahisha moyo, nao utamu wa mpenda mwenziwe, huu ndio unaotoka katika mashauri mema ya roho. Usimwache mwenzio wala mwenziwe baba yako! Wala mwake ndugu yako usimwingie siku, ulipopatwa na mabaya! Mtu akaaye karibu na mwema kuliko ndugu alioko mbali. Mwanangu, erevuka kweli, uufurahishe moyo wangu, nipate kumjibu mtu, akinitukana! Mwerevu wa kweli akiona mabaya kujificha, lakini wajinga hupita tu, wakapatwa nayo. Zichukue nguo zake yeye aliyejitoa kuwa dhamana ya mwingine, kwa ajili ya mwanamke mgeni mnyang'anye mali zake! Mtu akimbariki mwenziwe kwa sauti kuu asubuhi na mapema huwaziwa, ya kuwa amemwapiza. Maji yasiyokoma kuchuruzika toka mchirizini siku ya mvua nyingi na mwanamke mgomvi ni sawasawa; awezaye kumzuia aweza kuuzuia nao upepo, mkono wake wa kuume huweza kushika nayo mafuta yauingiayo. Chuma hunoa chuma; ndivyo, mtu na uso wa mwenziwe wanavyonoana. Alindaye mkuyu hula kuyu zake, naye awaangaliaye mabwana zake hupata macheo. Kama majini uso unayvoelekea uso, ndivyo, moyo wa mtu unavyouelekea moyo wa mwenziwe. Kuzimu nako, watu wanakopotelea, hakushibi, vivyo hivyo nayo macho ya watu hayashibi. Chungu cha kuyeyushia hujaribu fedha, nayo tanuru hujaribu dhahabu, lakini mtu hujaribiwa nayo, vinywa vya watu vinayomsifia. Ijapo umtwange mjinga kwa mchi katika kinu pamoja na mchele, ujinga wake hautamtoka. Sharti ujue vema, jinsi makundi yako yalivyo, kauelekeze moyo wako kuwaangalia nao ng'ombe! Kwani kilimbiko hicho nacho sicho cha kale na kale, au kiko kilemba cha kifalme kikaliachao vizazi na vizazi? Majani makavu yakiisha kuondolewa, hutokea mabichi, nako milimani hukusanywa majani mazuri ya kula. Wana kondoo hukupatia mavazi yako, nayo madume ni malipo ya kununua shamba. Tena yako maziwa ya mbuzi yatoshayo kukulisha wewe na kuwalisha nao waliomo nyumbani mwako, hata kuwa posho ya watumishi wako wa kike. Wasiomcha Mungu hukimbia pasipo kufukuzwa, lakini waongofu hutulia pasipo kustushwa kama mwana wa simba. Kwa ajili ya mapotovu ya nchi wakuu wake huwa wengi, lakini mtambuzi mwenye akili huitengemanisha siku nyingi. Mtu akosaye mali akikorofisha wanyonge, ni mvua ifurikayo pasipo kuleta chakula. Wayaachao Maonyo huwasifu wasiomcha Mungu, lakini wayaangaliao Maonyo huwakasirisha sana. Watu wabaya hawatambui mashauri yaliyo sawa, lakini wamtafutao Bwana huyatambua yote. Maskini ashikaye njia yake pasipo kukosa ni mwema kuliko apotoaye njia zake akipata mali nyingi. Ayashikaye Maonyo ni mwana wa mtambuzi, lakini aliye mwenzao walafi humtia baba yake soni. Ajipatiaye mali kwa kukopesha na kutaka faida nyingi huzikusanyia mwingine atakayezigawia wanyonge. Ayageuzaye masikio, yasisikie Maonyo, akimwomba Mungu hutapisha. Apotezaye waongofu, washike njia mbaya, hutumbukia mwenyewe katika shimo lake, lakini wasiokosa watapata mema, yawe mafungu yao. Mtu mkwasi ni mwerevu wa kweli machoni pake yeye, lakini mnyonge mwenye utambuzi humchunguza. Waongofu wakishangilia, uko utukufu mwingi, lakini wasiomcha Mungu wakipata ukuu, watu hujificha. Ayafichaye mpotovu yake hatafanikiwa, ayaungamaye na kuyaacha atahurumiwa. Mwenye shangwe ni mtu ajiangaliaye pasipo kukoma, lakini aushupazaye moyo wake huangushwa na mabaya. Simba angurumaye na chui atamaniye kula ni mtu asiyemcha Mungu akitawala watu wanyonge. Mkuu akosaye utambuzi huwakorofisha watu sana, lakini achukiaye mapato ya upotovu hukaa siku nyingi. Mtu alemewaye moyoni na damu ya mtu, aliyemwua, hutangatanga hata kuingia shimoni, asione wamshikizao. Aendeleaye pasipo kukosa huokoka, lakini ajipotoaye kwa kushika njia mbili, mara huanguka katika moja. Alilimiaye shamba lake hushiba chakula, lakini akimbiliaye mambo ya bure hushiba ukosefu. Mtu mwenye kweli hupata mbaraka nyingi, lakini ajihimizaye kupata upesi mali nyingi hakosi kukora manza. Kuzitazama nyuso za watu hakufai, lakini wako wajikoseshao kwa ajili ya kitonge cha wali. Ajikazaye sana kupata mali nyingi huwa mwenye jicho baya, hajui, ya kuwa ukosefu utamjia. Amwonyaye mtu mwisho atashukuriwa kuliko asemaye mororo kwa ulimi wake. Apokonyaye mali za baba na za mama na kusema: Huku siko kukosa, yeye ni sawa na mtu aangamizaye vibaya. Aliye na roho yenye tamaa nyingi huzusha magomvi, lakini amwegemeaye Bwana hushibishwa sana. Auegemeaye moyo wake yeye ni mpumbavu, lakini aendeleaye kwa werevu wa kweli yeye hupona. Amgawiaye mkosefu hataona ukosefu, lakini ayafumbaye macho yake huapizwa kabisa. Wasiomcha Mungu wakipata ukuu, watu hujificha, lakini wakiangamia, waongofu huongezeka. Mtu aonwaye akishupaza shingo mara atavunjika, asione atakayemponya. Waongofu wakipata nguvu, watu hufurahi, lakini asiyemcha Mungu akitawala, watu hupiga kite. Mtu apendaye werevu wa kweli humfurahisha baba yake, lakini mtu akiwa mwenzao wanawake wagoni huzipoteza mali. Mfalme huishikiza nchi yake kwa kupiga mashauri yaliyo sawa, lakini aitozaye kodi nyingi huiangamiza. Mtu amwambiaye mwenziwe maneno mororo humtegea tanzi, ainase miguu yake. lakini mwongofu hupiga shangwe kwa kufurahi. Mtu mbaya hujitegea mwenyewe kwa upotovu wake, lakini mwongofu hupiga shangwe kwa kufurahi. Mwongofu huyajua mashauri ya wanyonge, lakini asiyemcha Mungu hautambui huo ujuzi. Wenye ufyozaji huuchafua mji, lakini wenye werevu wa kweli huyatuliza makali. Mtu mwerevu wa kweli akishindana na mjinga, huyu hukasirika, tena hucheka, mambo yasipate kutulia. Wamwagao damu humchukia asiyekosa, lakini wanyokao hutafuta njia ya huiponya roho yake. Mpumbavu hutoa ukali wote wa roho yake, lakini mwerevu wa kweli huuzuia, apate kuunyamazisha. Mtawalaji akisikiliza maneno ya uwongo, watumishi wake wote huacha kumcha Mungu. Maskini na mkorofi hukutana, aliyewapa wote wawili mwanga wa macho ni Bwana. Mfalme akataye mashauri ya wanyonge kwa kweli, kiti chake cha kifalme kitashupaa kale na kale. Fimbo na mapigo humwerevusha mtu kweli, lakini mwana aliyeachiliwa tu humtia mama yake soni. Wasiomcha Mungu wakipata nguvu, wapotovu huwa wengi, lakini waongofu hufurahia maanguko yao. Mchape mwanao! Ndivyo, atakavyokupatia utulivu akiifurahisha roho yako vizuri. Pasipo kufumbuliwa mambo watu hawazuiliki, lakini ayaangaliaye Maonyo hufanikiwa. Kwa maneno tu mtumishi haonyeki, kwani huyatambua, lakini hayatii. Ukiona mtu ajihimizaye kusema maneno, basi, mpumbavu huegemeka kuliko huyo. Mtu akimtunza mtumishi wake kwa upole tu toka utoto, mwisho yeye atakuwa kibwana. Mtu mkali huzusha magomvi, naye akasirikaye upesi hufanya mapotovu mengi. Majivuno humnyenyekeza mtu, lakini anyenyekeaye rohoni hupata macheo. Afanyaye bia na wezi hujichukia mwenyewe, akisikia maapizo hamjulishi aliyeapizwa. Kuogopa watu ni kujitegea tanzi, lakini amwegemeaye Bwana hulindwa. Wengi hutafuta upendeleo wa mtawalaji, lakini kwake Bwana kila mtu huyapata yampasayo. Mtu mwovu hutapisha waongofu, naye ashikaye njia inyokayo humtapisha asiyemcha Mungu. Mtu husema: Nimejisumbua, Mungu, kweli nimejisumbua, Mungu, nikawezekana. Mimi ninapumbaa kama nyama, utambuzi wa kimtu sinao. Sikujifunza werevu wa kweli, nimjue Mtakatifu, kama wengine wanavyomjua. Ni nani aliyepaa mbinguni, ashuke chini? Ni nani aukusanyaye upepo magaoni mwake? Ni nani aliyeyafunga maji katika vazi lake? Ni nani aliyeyashupaza mapeo yote ya nchi? Jina lake ni nani? Tena jina la mwanawe ni nani? Unayajua wewe? Kila neno la Mungu ni nguvu, ni ngao yao wamkimbiliao. Maneno yake usiyaongeze kwa kutia jingine, asije kukukanya, ukajulikana kuwa mwongo. Ninakuomba maneno haya mawili, usininyime hayo, nikiwa ningaliko sijafa bado. Yaliyo upuzi na maneno ya uwongo yaweke mbali yasinifikie! Usinipe kuwa mkosefu wa mali wala mwenye mali nyingi! Ila nipe tu, nile chakula changu kinipasacho! Nisije kwa kushiba, nikabisha kwamba: Bwana ni nani? Wala nisije kwa ukosefu, nikaiba, nikalikosea Jina la Mungu wangu. Usimsingizie mtumishi kwa bwana wake, asikuapize, ukajipatia mapatilizo. Kiko kizazi cha watu wawaapizao baba zao, wasiwabariki wamama zao. Kiko kizazi cha watu waliotakata machoni pao wenyewe, nao hawakujiosha, uchafu wao uwatoke. Kiko kizazi cha watu walio wakuu zaidi machoni pao wenyewe, nazo kope za macho yao huelekezwa juu sana. Kiko kizazi cha watu wenye panga kuwa meno yao, wenye majisu kuwa magego yao, hutaka kuwala wanyonge, watoweke katika nchi, nao wakiwa, watoweke katika watu. Mruba ana wana wawili wa kike: Nipe! Nipe! Viko vitu vitatu visivyoshiba, tena vinne visivyosema: Basi. Ni kuzimu na tumbo lisilozaa, ni nchi isiyoshiba maji na moto usiosema: Basi. Jicho la mtu amfyozaye baba yake, akakataa kumtii mama yake, sharti kunguru waling'oe mtoni, liliwe na makinda ya kozi. Yako mambo matatu, ninayoyastaajabu sana, tena yako manne, nisiyoyajua maana: njia ya tai angani na njia ya nyoka mwambani na njia ya merikebu baharini na njia ya mtu na mwanamwali. Ndivyo, njia ya mwanamke mgoni ilivyo: hula, kisha hufuta kinywa chake na kusema: Sikukosa neno. Yako mambo matatu yanayoitetemesha nchi, tena yako manne, nchi isiyoweza kuyavumilia: ni mtumwa akipata ufalme, ni mpumbavu akishiba sana vyakula, ni mwanamke aliyechukizwa akiolewa, ni mjakazi akizipata mali za bibi yake, ziwe fungu lake. Wako nyama wanne walio wadogo katika nchi kuliko wengine, nao ni werevu walioerevuka kweli. Ni siafu: kweli hawana nguvu, lakini huvitengneza vyakula vyao siku za mavuno yao. Ni pelele: wao si wenye nguvu, lakini huweka nyumba zao magengeni. Ni nzige: hawana mfalme, lakini hutoka wote pia vikosi kwa vikosi. Ni mijusi: mtu anaweza kuwakamata kwa mikono, lakini namo majumbani mwa wafalme wamo. Wako watatu wenye mwendo upendezao, tena wako wanne wenye mwendo mzuri. Ni simba awapitaye nyama wote nguvu, harudi nyumba kwa kuona cho chote. Ni farasi mwenye matandiko kiunoni, ni beberu naye, tena ni mfalme akiviongoza vikosi vyake. Kama umepumbaa kwa kujikuza, au kama umewaza mabaya moyoni, kifumbe kinywa kwa kukibandikia mkono! Kwa kusukasuka maziwa huleta siagi, tena kuzidi kukamua pua hutoa damu, nako kuchochea makali huleta ugomvi. Maneno ya mfalme Lemweli wa Masa, mama yake aliyomfunza. Niseme nini, mwanangu? Niseme nini, mwanangu, niliyekuzaa? Niseme nini, mwanangu, niliyemwapia viapo? Usiwape wanawake nguvu zako! Wala usizishike njia zao, maana huangamiza wafalme. Wafalme, Lemweli, wafalme hawapaswi na kunywa mvinyo, wala wakuu haiwapasi kuuliza: Vileo viko wapi? Wasije kusahau maongozi kwa kunywa kwao, wakayapotoa mashauri yao wote walio wanyonge. Wapeni vileo wanaokwenda kujipoteza, wapeni mvinyo walio wenye uchungu rohoni mwao! Wanywe, wakausahau umaskini wao, wasiyakumbuke tena masumbuko yao! Kifunue kinywa chako kuwatetea wasioweza kusema, uwasaidie shaurini wote walioachwa peke yao! Kifunue kinywa chako, ukate mashauri yaongokayo, uwapatie wanyonge na maskini shaurini yawapasayo. Yuko nani aonaye mwanamke mwenye uwezo mwema? Kima chake ni kikubwa kuliko kina cha lulu. Moyo wa mumewe huweza kumtegemea, nayo mapato hayakoseki. Humfanyizia mema tu, mabaya hayafanyi siku zote za maisha yake. Hutafuta manyoya ya kondoo na pamba, kisha hufanya kazi za kuzitumia kwa mikono ipendayo kufanya kazi. Hufanana na merikebu za mchuuzi, akileta vyakula vyake toka mbali. Huamka usiku, ukiwa haujaisha bado, huwapa chakula waliomo nyumbani mwake, nao vijakazi huwapa kazi ziwapasazo. Akiviwaza moyoni kuwa vema hivyo hununua shamba, tena hupanda mizabibu kwa mapato ya mikono yake. Hujifunga kiunoni kwa nguvu, kisha huishupaza mikono yake, ifanye kazi. Huona, ya kuwa anafanikiwa vema kwa kujikaza hivyo, kwa hivyo hata usiku taa yake haizimiki. Hutengeneza kitanda cha kufumia kwa mikono yake, kisha vidole vyake huvifumisha nguo. Wanyonge huwashika kwa mkono wake, nao wakiwa huwapokea kwa mikono yake miwili. Haogopi, ya kuwa baridi kali iwapate waliomo nyumbani mwake, kwani wa nyumbani mwake wote hupata mavazi mekundu ya sufi. Hujitengenezea mazulia, hujivika nguo nzuri za pamba, hata za rangi. Mumewe hujulika malangoni mashaurini akikaa pamoja na wazee wa nchi. Hutengeneza fulana, akaziuza, nayo mishipi huwapa wachuuzi. Uwezo na utukufu ndio mavazi yake, kwa hiyo huyacheka mambo ya siku ijayo. Kinywa hukifunua, kiseme maneno yenye werevu wa kweli, nayo maonyo yenye upole yamo katika ulimi wake. Huangalia sana mwenendo wao waliomo nyumbani mwake, vilaji vya uvivu havili kabisa. Wanawe hutokea na kumtukuza, mumewe naye humshangilia kwamba: Wako wanawake wengi wenye uwezo wa kufanya mema, lakini wewe umewapita wote pia. Upendezi hudanganya, nao uzuri ni wa bure, lakini mwanamke amchaye Bwana hupasa kutukuzwa. Mpeni mapato ya mikono yake, matendo yake yamtukuze malangoni! Haya ni maneno ya Mpiga mbiu, mwana wa Dawidi, mfalme wa Yerusalemu. Mpiga mbiu asema: Yote ni ya bure kabisa, kweli yote ni ya bure kabisa, yote pia ni ya bure. Mtu hupata nini kwa masumbuko yake yote, anayojisumbua chini ya jua? Kizazi kimoja kikienda zake, kingine huja, lakini nchi hukaa kale na kale. Jua hucha, tena huchwa, kisha hupakimbilia pake pa macheo yake. Upepo ukienda kusini, kisha hugeuka kwenda kaskazini; ndivyo, upepo unavyojiendea na kugeukageuka. Kwa kugeukageuka kwake upepo hurudia hapo, ulipotokea. Mito yote huenda baharini, lakini bahari haijai; papo hapo, mito inaposhika njia zao, ndipo, inapojiendea na kuishika njia ileile. Mambo yote huchokesha, mtu asiweze kuyasema yote, wala macho hayashibi kwa kuyatazama, wala masikio hayajai kwa kuyasikia. Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako tena, nayo yaliyofanywa ndiyo yatakayofanywa tena; hakuna jipya litakalotokea chini ya jua. Kama litatokea, watu wanalotaka kulisema kwamba: Hili ni jipya kweli, limekwisha kuwako siku za kale kabisa zilizokuwako mbele yetu. Ni hivyo tu, wa kwanza hawakumbukwi, vivyo nao wa nyuma watakaokuwako hawatakumbukwa kwao watakaokuwako nyuma yao. Mimi Mpiga mbiu nilikuwa mfalme wa Isiraeli huko Yerusalemu. Nikajipa moyo, kuyatafuta na kuyapeleleza kwa werevu wa kweli yote pia yanayofanyika chini ya mbingu; ni sumbuko baya, Mungu alilowapa wana wa Adamu kulisumbukia. Nikayatazama yote yanayofanywa chini ya jua, nikayaona yote kuwa ya bure, kuwa kuukimbilia upepo. Yapotokayo hayanyosheki, wala yasiyokuwako hayahesabiki. Naliwaza moyoni mwangu kwamba: Mimi nimejipatia werevu wa kweli mwingi, nikauongeza kuwa mwingi zaidi kuupita wa watu wote waliokuwako mbele yangu Yerusalemu, kweli moyo wangu ulipata werevu wa kweli na juzi mwingi. Lakini nilipojipa moyo kujua, jinsi werevu wa kweli ulivyo, tena kujua, jinsi upumbavu na ujinga ulivyo, ndipo, nilipojua, ya kuwa hayo nayo ni kuukimbilia upepo. Kwani werevu mwingi ulipo, yapo nayo masikitiko mengi, naye aongoezaye ujuzi huongeza nayo maumivu. Nilisema moyoni mwangu: Haya! Niyajaribu yenye furaha, nijionee mema! Nikaona, hayo nayo ni ya bure. Macheko nikayaambia: Ni kuwa na wazimu, nayo furaha nikaiambia: Hii inafaaje? Niliwaza moyoni mwangu kuufurahisha mwili wangu kwa mvinyo, lakini akili zikae zikiuongoza mwili; nikataka kuufuata huo ujinga, mpaka niyaone yawafaliayo wana wa Adamu kuyafanya chini ya mbingu siku zao zote za kuwapo. Matendo yangu, niliyoyafanya, yakawa makubwa: nilijijengea nyumba, nikajipandia mizabibu. Nikajitengenezea mashamba na vimwitu, nikapanda humo miti ya matunda ya kila namna. Nikajitengenezea nayo maziwa ya maji ya kunyweshea mwitu, uichipuze miti. Nikajipatia watumishi na vijakazi, nikawa nao watumwa waliozaliwa nyumbani mwangu, nikawa na makundi ya ng'ombe na ya kondoo kuliko wote waliokuwako mbele yangu Yerusalemu. Nikajikusanyia nazo fedha na dhahabu zilizokuwa mali za wafalme wengine na za nchi nyingine, nikajipatia waimbaji waume na wake, tena wana wa Adamu wanaowatunukia sana, mabibi wengi sana. Hivyo nikawa mkuu zaidi kuwashinda wote pia waliokuwako mbele yangu Yerusalemu, nao werevu wangu wa kweli ukakaa kwangu. Yote, macho yangu yaliyoyatamani, hakuna nilichoyanyima; wala moyo wangu sikuukataza furaha yo yote. Kwani moyo wangu uliyafurahia yote, niliyoyasumbukia, tena furaha hii ilikuwa pato langu, nililojipatia kwa masumbuko yangu yote. Lakini nilipogeuka kuzitazama kazi zote, mikono yangu ilizozifanya, tena nilipoyakumbuka hayo masumbuko, niliyoyasumbuka kwa kuyafanya yale, ndipo, nilipoona, yote ni ya bure, ni kuukimbilia upepo, hakuna pato, mtu analojipatia chini ya jua. Kisha mimi nikageuka kuupambanua werevu wa kweli na upumbavu na ujinga; kwani mtu atakayemfuata mfalme atafanya nini? Ni yale yale, watu waliyoyafanya tangu kale. Mimi nikatazama, kama liko, ambalo werevu wa kweli unaupita ujinga, nikaona kuwa sawa, kama mwanga unavyoipita giza. Mwerevu wa kweli anayo macho yake kichwani mwake, naye mjinga huenda gizani; lakini papo hapo nikatambua nayo haya, ya kuwa jambo la mwisho linalowapata wao wote ni lilo hilo moja. Nikasema moyoni mwangu: Kama jambo la mwisho linalompata mjinga ni lilelile litakalonipata mimi nami, werevu wangu wa kweli uliozidi sana ni wa nini? Nikasema moyoni mwangu: Huu nao ni wa bure. Kwani wala mwerevu wa kweli wala mjinga atakumbukwa kale na kale; kwani katika siku zijazo wote pia watakuwa wamesahauliwa. Kumbe mwerevu wa kweli hufa sawasawa kama mjinga! Nikachukizwa na kuwapo, kwani kazi zinazofanywa chini ya jua zikawa mbaya machoni pangu, kwani zote ni za bure, ni za kuukimbilia upepo. Ndipo, mimi nilipochukizwa na masumbuko yangu yote niliyoyasumbuka chini ya jua, kwani niliyoyasumbukia nitamwachia mtu atakayekuwapo nyuma yangu. Tena yuko nani anayejua, kama atakuwa mwerevu wa kweli au mjinga? Lakini atayatawala yote, niliyojipatia chini ya jua kwa usumbufu wangu na kwa werevu wangu wa kweli. Kwa hiyo nayo ni ya bure. Ndipo, nilipotangatanga na kuzikata tamaa zote za moyo wangu kwa ajili ya masumbuko, niliyoyasumbuka chini ya jua. Kwani huwa hivyo: mtu aliyejisumbua kwa werevu wa kweli na kwa ujuzi na kwa kufanikiwa humpa fungu lake mtu asiyelisumbukia. Hayo nayo ni ya bure na mabaya sana. Kwani kiko kitu gani, mtu anachokipata kwa masumbuko yake yote na kwa bidii za moyo wake, ulizozifanya na kusumbuka chini ya jua? Kwani siku zake zote ni za maumivu, nao utumishi wake ni wenye masikitiko, moyo wake usiweze kutulia nao usiku; hayo nayo ni ya bure. Basi, hakuna mema ya mtu kuliko kula na kunywa na kuipatia roho yake mema katika masumbuko yake. Lakini haya nayo nikayaona, ya kuwa hutoka mkononi mwa Mungu tu. Kwani yuko nani awezaye kula na kujifurahisha, huyu akiwa hayuko? Kwani mtu aliye mwema machoni pake humpa werevu wa kweli na ujuzi na furaha; lakini aliye mkosaji humpa utumishi wa kukusanya na kulimbika, ampe yule aliye mwema machoni pake Mungu. Hayo nayo ni ya bure na kuukimbilia upepo. Kila jambo lina saa yake, kila jambo lipendezalo chini ya mbingu lina wakati wake: Kuzaliwa kuna wakati wake, nako kufa kuna wakati wake; kupanda kuna wakati wake, nako kuyang'oa yaliyopandwa kuna wakati wake. Kuua kuna wakati wake, nako kuponya kuna wakati wake; kubomoa kuna wakati wake, nako kujenga kuna wakati wake. Kulia kuna wakati wake, nako kucheka kuna wakati wake; kuomboleza kua wakati wake, nako kucheza kuna wakati wake. Kutupa mawe kuna wakati wake, nako kukusanya mawe kuna wakati wake; kukumbatiana kuna wakati wake, nako kukataa kukumbatiana kuna wakati wake. Kutafuta kuna wakati wake, nako kupoteza kuna wakati wake; kuweka kuna wakati wake, nako kutupa kuna wakati wake. Kurarua kuna wakati wake, nako kushona kuna wakati wake; kunyamaza kimya kuna wakati wake, nako kusema kuna wakati wake. Kupendana kuna wakati wake, nako kuchukiana kuna wakati wake; kupigana kuna wakati wake, nako kutengemana kuna wakati wake. Afanyaye kazi analo pato gani kwa kusumbuka kwake? Nikautazama utumishi, Mungu aliowapa wana wa Adamu kuutumikia. Yote aliyafanya kuwa mazuri wakati wao, akawapa kuziwaza mioyoni mwao nazo siku zijazo; ni hiyo tu, asiyowapa: mtu asiione maana ya kazi, Mungu aliyoifanya toka mwanzo hata mwisho. Ndipo, nilipojua, ya kuwa hakuna lililo jema kwao kuliko kufurahi na kufanya mema siku zao za kuwapo. Haya nayo nikayajua, ya kuwa kwake kila mtu apataye kula na kunywa na kuona mema kwa masumbuko yake, hiki nacho ni kipaji cha Mungu. Nikajua, ya kuwa yote, Mungu ayafanyayo, hukaa kale na kale; hapo hapana kuongeza wala kupunguza, kwani Mungu aliyafanya kuwa hivyo, watu wamwogope. Yaliyoko yalikuwako kale, nayo yatakaokuwako yalikuwako kale. Naye Mungu huyazusha yaliyopitishwa. Tena niliona, ya kuwa chini ya jua uko upotovu penye mashauri yanyokayo, napo penye wongofu uko upotovu. Ndipo, niliposema moyoni mwangu: Mungu atamhukumu mwongofu pamoja na mpotovu, kwani kila jambo lipendezalo aliliwekea wakati wake, hata matendo yote. Nikasema moyoni mwangu; Ni kwa ajili ya wana wa Adamu, Mungu akitaka kuwajaribu, waone, ya kuwa wao na nyama ni sawa. Kwani jambo la mwisho linalowapata wana wa Adamu nalo jambo la mwisho linalowapata nyama ni jambo lilo hilo moja; kama huyu anavyokufa, ndivyo, yule naye anavyokufa, pumzi yao wote ni moja tu. Kwa hiyo haliko, mtu analompita nyama, kwani yote ni ya bure. Wote pia hupaendea mahali pale pamoja: wote walitoka uvumbini, tena wote hurudi uvumbini. Yuko nani ajuaye, kama roho za wana wa Adamu hupaa juu? au kama roho za nyama hushuka chini kuzimuni? Ndivyo, nilivyoona, ya kuwa hakuna mema, mtu ayapatayo kuliko kuzifurahia kazi zake, kwani hili ndilo fungu lake yeye. Kwani yuko nani atakayempeleka mahali, atakapoyaona. Nilipoyatazama tena makorofi yanayofanywa chini ya jua, niliona machozi yao waliokorofishwa, lakini sikuona aliyewatuliza mioyo; namo mikononi mwao waliowakorofisha zimo nguvu, kwa hiyo kwao hakuna atakayewatuliza mioyo. Kwa sababu hii nikawawazia wafu waliokufa kale kuwa wenye shangwe kuliko wao wanaoishi bado wenye maisha. Lakini niliyemwazia kuwa amepata mema kuliko wao wote wawili, ni yule asiyepata bado kuzaliwa, kwa kuwa hakuyaona hayo matendo mabaya yanayofanywa chini ya jua. Tena niliona, ya kuwa masumbuko yote na kufanikiwa kote katika kazi hutoka katika wivu, mtu anaomwonea mwenziwe; hayo nayo ni ya bure na kuukimbilia upepo. Mjinga hukaa na kuifunga mikono yake; basi, hujila mwenyewe. Kiganja kimoja kikijaa matulivu ni vema kuliko magao yote mawili yakijaa masumbufu ya kuukimbilia upepo. Nikatazama na mengine yaliyo ya bure chini ya jua: kama mtu yuko peke yake pasipo mwenziwe wa pili wala mwana wala ndugu, hakomi kabisa kujisumbua, wala jicho lake halishibi kuzitazama mali, naye husema: Mimi ninamsumbukia nani na kujinyima mwenyewe mema yote? Basi, hayo nayo ni ya bure na utumishi mbaya. Kuwa wawili kunafaa kuliko kuwa mmoja tu, kwa kuwa hao hupata mshahara mwema wa masumbuko yao. Kwani wakianguka, mmoja humwinua mwenziwe lakini mtu aliye peke yake akianguka, ni vibaya, maana hana mwenziwe wa kumwinua. Tena wawili wakilala pamoja hutiana jasho; lakini aliye peke yake atawezaje kupata jasho? Tena aliye peke yake mtu humshinda, lakini wawili wataweza kusimama mbele yake. Nayo kamba yenye nyuzi tatu haikatiki upesi. Kijana mkiwa mwenye werevu wa kweli ni mwema kuliko mfalme mzee, akiwa mjinga asiyejua kuonyeka tena. Kwani itakuwa, yule atoke kifungoni, apate ufalme, naye aliyezaliwa katika ufalme wake awe mkiwa. Nikawaona wote walioishi na kutembea chini ya jua, wakirudi upande wa huyo kijana wa pili aliyesimama mahali pake yule. Nao watu wote, aliowaongoza wote pia, hawakuhesabika. Lakini watakaokuwako nyuma yake hawatamfurahia. Kwa hiyo nayo yalikuwa ya bure na kuukimbilia upepo. Iangalie miguu yako ukienda Nyumbani mwa Mungu, uje kusikia! Hii inafaa kuliko vipaji vya tambiko, wajinga wanavyovitoa, kwani wao hawajui, ya kuwa hufanya mabaya. Usibabaike tu kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe mwepesi wa kutoa maneno mbele ya Mungu! Kwani Mungu yuko mbinguni, wewe nawe uko huku nchini, kwa hiyo maneno yako sharti yawe machache. Kwani ndoto huja kwa kutumikia mengi, nayo sauti ya mjinga kujulika kwa kusema maneno mengi. Kama umemwapia Mungu kiapo cho chote, usikawe kukilipa! Kwani hapendezwi na wajinga; cho chote, ulichokiapa, kilipe! Ukiwa hukuapa, ni vema, kuliko ukiwa hukilipi, ulichokiapa. Usiache, kinywa chako kiukoseshe mwili wako, wala usimwambie malaika: Hili ni kosa tu! Unataka kwa nini, Mungu ayakasirikie, uliyoyasema, kisha aziangamize kazi za mikono yako? Kwani ndoto zikiwa nyingi, nayo maneno yakiwa mengi, mengi ni ya bure; kwa hiyo umwogope Mungu! Ukiona, maskini akikorofishwa, tena mashauri yaliyo sawa nayo mambo yaongokayo yakiondolewa mjini kwa nguvu, usivistaajabu, vikifanyika hivyo! Kwani aliye mkuu yuko na mkuu kumpita amwangaliaye, tena juu yao wote yuko aliye mkuu mwenyewe. Kwa ajili ya hayo yote inafaa, nchi ikiwa na mfalme ayatazamaye mashamba, yalimwe. Apendaye fedha hashibi fedha, wala apendaye mali hatoshewi na mapato. Hayo nayo ni ya bure. Mema yakiwa mengi, basi, nao watakao kuyala huwa wengi; naye mwenyewe hupata nini, isipokuwa hii tu, macho yake yakiyatazama kwa kufurahi. Usingizi wa mtu wa kazi ni mtamu, kama anakula vichache au vingi; lakini shibe za mkwasi hazimpatii mapumziko ya kulala usingizi. Uko ubaya unaouguza, nami nimeuona chini ya jua, ni huu: mali zilizoangaliwa na mwenyewe mwisho zikimpatia mabaya. Mali hizo zikipotea kwa kutumikiwa vibaya, naye akiwa amezaa mtoto, basi, hakuna hata kidogo kitakachokuwa mkononi mwake. Vivyo hivyo, alivyotoka tumboni mwa mama yake mwenye uchi, ndivyo, atakavyokwenda tena, kama alivyokuja, asichukue kwa masumbuko yake cho chote cha kwenda nacho mkononi mwake. Kweli huu ndio ubaya uuguzao. Vivyo hivyo, alivyokuja, ndivyo, atakavyokwenda; tena anapataje kwa kuusumbukia upepo? Naye siku zake zote alizila na kukaa gizani mwenye masikitiko mengi kwa kuugua na kwa kukasirika. Yasikie, niliyoyaona kuwa mema na mazuri! Ni haya: mtu akila, akinywa na kuona mema kwa masumbuko yake, aliyoyasumbuka chini ya jua siku zote za maisha yake, Mungu alizompa, kwani hili ndilo fungu lake. Tena mtu ye yote, Mungu aliyemgawia mali na mema ya dunia hii na kumpa uwezo wa kuyala na kulichukua fungu lake na kuyafurahia masumbuko yake, basi, ajue, ya kuwa hilo ndilo gawio lake Mungu. Kwani huyu hakumbuki kabisa, jinsi siku zake za kuwapo zilivyo, kwani Mungu humwitikia kwa kuufurahisha moyo wake. Yako mabaya, niliyoyaona chini ya mbingu, nayo huwalemea watu sana. Mungu akimgawia mtu mali na mema ya dunia hii na macheo, asijinyime lo lote, moyo wake ulitunukialo, lakini Mungu asipompa uwezo wa kuyala, ila mgeni akiyala, basi, yanamwia ya bure, tena humwuguza vibaya. Mtu akizaa watoto mia, miaka ya maisha yake ikawa mingi, siku za miaka yake zikihesabiwa ziwe nyingi kweli, lakini roho yake isipoyashiba hayo mema yake, naye asipate hata kaburi, basi, nasema: Mtoto aliyekufa katika kuzaliwa alipata mema kuliko yeye. Kwani huyo mtoto huja kama si kitu, huenda gizani, nalo jina lake limo gizani. Jua tu hakuliona, wala halijui; lakini hutulia kuliko yule. Kama mtu angepata kuwapo miaka elfu mbili, asione mema, huyu naye haendi mahali pale pamoja, wote wanapokwenda? Masumbuko yote ya mtu ni ya kukijaza kinywa chake, lakini hivyo roho yake haishibi. Kwani yako mapato gani, mwerevu wa kweli anayoyapata, mjinga asiyoyapata? Au yako mapato gani, mnyonge anayoyapata akijua mwenendo ufaao machoni pa watu wanaoishi? Kuyatazama yaliyoko machoni ni kwema kuliko kwenda na kuzifuata tamaa; hayo nayo ni ya bure na kuukimbilia upepo. Yaliyoko yamekwisha kuitwa jina tangu kale, nayo yatakayompata mtu yamekwisha kujulikana kale; hakuna mtu anayeweza kubishana na mwenziwe amshindaye nguvu. Kwani yako mambo mengi yaletayo mengi yaliyo ya bure; hayo mtu yanamfalia nini? Kwani yuko nani ayajuaye yamfaliayo mtu huku nchini siku hizi za kuwapo zinazohesabika, zilizo za bure tu? maana huzila kama kivuli. Yuko nani awezaye kumwelezea mtu yatakayokuwako nyuma yake chini ya jua? Jina zuri ni jema kuliko mafuta mazuri, nayo siku ya kufa ni njema kuliko siku ya kuzaliwa. Kuingia nyumbani mwenye matanga ni kwema kuliko kuingia nyumbani mwenye watu wanywao, kwa kuwa mle huelekea mwisho wa watu wote, naye mwenye uzima huyaweka moyoni. Masikitiko ni mema kuliko macheko, kwani uso ukiwa mbaya, moyo huwa mwema. Mioyo ya werevu wa kweli huwa nyumbani mwenye matanga, lakini mioyo ya wajinga huwa nyumbani mwenye furaha. Kuyasikiliza makemeo ya mwerevu wa kweli ni kwema, kuliko mtu akizisikiliza nyimbo za wajinga. Kwani kama moto wa miiba unavyovuma chini ya chungu, ndivyo, macheko ya mjinga yalivyo; hayo nayo ni ya bure. Kweli ukorofi humpumbaza mwerevu wa kweli, nayo mapenyezo huzipoteza akili. Mwisho wa jambo ni mwema kuliko mwanzo wake; mwenye uvumilivu ni mwema kuliko mwenye majivuno. Usiwe mwepesi wa kukasirika rohoni mwako; kwani makasiriko hutua kufuani mwa mjinga. Usiulize kwamba: Inakuwaje, siku za kale zikiwa njema kuliko hizi za sasa? Kwani huulizi hivyo kwa kuwa mwenye werevu wa kweli. Werevu wa kweli ni mwema kama fungu uliloachiwa, tena ni pato kwao walionao jua. Kivulini kwa werevu wa kweli ni kuzuri kama kivulini kwa fedha, lakini ujuzi hushinda, kwa kuwa werevu wa kweli huwapatia wenyewe uzima. Yatazame matendo yake Mungu! Kwani yuko nani awezaye kuyanyosha aliyoyapotoa? Siku ikiwa njema, nawe furahiwa! Lakini siku ikiwa mbaya, jiangalie! Kwani hii nayo Mungu ameifanya, kama alivyoifanya ile, kwa kwamba: Mtu asione cho chote kitakachokuwako nyuma yake. Haya yote mawili niliyaona katika siku zangu zilizo za bure nazo: wako waongofu wanaoangamia, ijapo wawe wenye wongofu, tena wako wasiomcha Mungu wanaokaa siku nyingi, ijapo wawe wenye ubaya. Usiuzidishe wongofu, wala usijipatie werevu wa kweli kushinda wengine! Kwa nini unataka kujiangamiza? Tena usizidishe uovu, wala usiwe mjinga! Kwa nini unataka kufa, siku zako zikiwa hazijatimia bado? Ni vema, ushike upande huu! Lakini napo penye upande mwingine usiuondoe mkono wako! Kwani amchaye Mungu huyapona yote mawili. Werevu wa kweli humtia mwerevu wa kweli nguvu zaidi kuliko wakuu kumi watawalao mjini. Kwani huku nchini hakuna mtu mwongofu afanyaye mema tu pasipo kukosa. Tena usiyaangalie maneno yote, watu wanayoyasema, usije kumsikia mtumishi wako, akikutukana! Kwani moyo wako unajua, ya kuwa nawe mara nyingi ulitukana wengine. Hayo yote niliyajaribu kwa werevu wa kweli, nikasema: Na nierevuke kweli! Lakini werevu wa kweli hunikalia mbali. Iliyokuwa sababu yao ya kuwa hivyo iko mbali, tena imefichika sanasana, atakayeivumbua yuko nani? Nikazunguka, moyo wangu upate ujuzi na uchunguzi kwa kuutafuta werevu wa kweli na utambuzi, ujue, ya kuwa kumwacha Mungu ni ujinga, nao ujinga ndio upumbavu. Ndipo, nilipoona yaliyo yenye uchungu kuliko kufa, ndio mwanamke, moyo wake ukigeuka kuwa tanzi na wavu, nayo mikono yake ikiwa pingu. Mtu aliye mwema machoni pake Mungu huponyoka kwake, lakini mkosaji hunaswa naye. Mpiga mbiu akasema: Yatazame, niliyoyaona kwa kuunganisha moja kwa moja, nipate kuyatambua yaliyo kweli! Liko moja, roho yangu ililolitafuta pasipo kuliona: Mwanamume nimemwona mmoja katika elfu, lakini mwanamke, niliyemtafuta, sikumwona katika wao wote. Lakini hili moja, nililoliona, litazame nalo: Mungu alimwumba mtu kuwa mwongofu, lakini wao hutafuta mizungu mingi! Aliye kama mwerevu wa kweli ni nani? Tena yuko nani ajuaye maana ya mambo? Werevu wa kweli wa mtu huuangaza uso wake, ushupavu wa uso wake ugeuzwe. Mimi husema: Kiangalie kinywa cha mfalme, kwa kuwa uliapa na kumtaja Mungu! Usitoke upesi usoni pake, wala usishikamane na shauri baya! Kwani yeye hufanya yote yampendezayo. Kwa kuwa neno la mfalme lina nguvu, yuko nani awezaye kumwambia: Unafanya nini? Aishikaye amri yake hataona baya lo lote; nao moyo wa mwerevu wa kweli hujua, siku za wakati wa kukatia shauri zitakapotimia. Kwani kila jambo liko na siku zake za kukatiwa shauri. Kwani huu ndio ubaya unaowalemea watu sana: kwa kuwa hayuko ayajuaye yatakayokuwako, yuko nani atakayewaeleza, jinsi yatakavyokuwa? Hakuna mtu autawalaye upepo, aweze kuukomesha upepo, wala hakuna aitawalaye siku ya kufa, wala hakuna apewaye ruhusa siku ya mapigano; vivyo hivyo kumwacha Mungu hakuwaponyi wao waliomwacha. Hayo yote niliyatazama, nikayaweka moyoni mwangu, nikaziangalia kazi zote zinazofanywa chini ya jua, mtu anapomtawala mtu mwenziwe, apate kumfanyizia mabaya. Nikaona, wasiomcha Mungu wakizikwa, wafike pao; nao waliofanya yaliyopasa hawakuwa na budi kuondoka mahali patakatifu, wakasahauliwa mle mjini. Hayo nayo ni ya bure. Kwa kuwa patilizo la tendo baya halitimizwi upesi, kwa hiyo mioyo ya wana wa Adamu huzidi kufanya mabaya; tena ni kwa hiyo, mwenye kukosa na kufanya mabaya akipata kukaa siku nyingi. Lakini hayo nayo mimi ninayajua, ya kuwa wamchao Mungu wataona mema, kwa kuwa huucha uso wake. Lakini asiyemcha Mungu hataona mema, wala hatakaa siku nyingi, ila huwa kama kivuli tu, kwa kuwa hauchi uso wake. Yako yaliyo ya bure yanayofanyika huku nchini, ni haya: wako waongofu wanaopatwa na mambo yapasayo matendo yao wasiomcha Mungu; tena wako wasiomcha Mungu wanaopatwa na mambo yapasayo matendo yao waongofu. Nasema: Hayo nayo ni ya bure. Kwa hiyo nikaisifu furaha, kwa kuwa chini ya jua mtu hawezi kuona yaliyo mema kuliko kula na kunywa na kufurahi; haya na yafuatane naye kwa hivyo, anavyosumbuka siku zake za kuwapo chini ya jua, Mungu alizompa. Mara kwa mara nikauelekeza moyo wangu, uujue werevu wa kweli kwa kuzitazama kazi za utumishi zinazofanywa huku nchini, kwani wako wasioona usingizi machoni pao mchana wala usiku. Ndipo, nilipozitazama kazi zote za Mungu, nikaona, ya kuwa mtu hawezi kuzitambua maana hizo kazi zinazofanywa chini ya jua; ijapo mtu ajisumbue sana kwa kuitafuta hiyo maana, haioni. Hata mwerevu wa kweli akijiwazia kwamba ameijua, hawezi kuitambua. Hayo yote nikayaweka moyoni mwangu na kuyachunguza haya yote, ya kuwa waongofu na werevu wa kweli pamoja na kazi zao zote wamo mkononi mwa Mungu. Hakuna mtu ajuaye, kama ni kupenda au kama ni kuchukia kumpasako, yote pia yako yamefichika bado mbele yake. Kwani yote huwapata wote sawasawa, jambo lao la mwisho ni lilo hilo moja, humpata mwongofu naye asiyemcha Mungu, vilevile mwema atakataye naye mchafu, atambikaye naye asiyetambika, mwema na mkosaji, aapaye naye aogopaye kuapa; yote yanayofanywa chini ya mbingu yako na ubaya huu, jambo la mwisho likiwa lilelile moja kwao wote; tena ni huu, mioyo ya wana wa Adamu ikijaa mabaya, mumo humo mioyoni mwao mkikaa upumbavu siku za maisha yao, kisha huenda kwao wafu, ndio mwisho wao. Mtu akingali mwenye bia nao wote walio hai hutegemeka, kwani mbwa aliye hai hupata mema kuliko simba aliyekufa. Kwani walio hai hujua, ya kuwa watakufa, lakini wafu hawajui cho chote, tena hakuna mshahara wo wote, watakaoupata, kwani hawakumbukwi tena, wamekwisha kusahauliwa. Nao upendo wao na uchukivu wao na wivu wao ulitoweka kale, kale na kale hawana fungu lo lote tena katika mambo yote yanayofanywa chini ya jua. Jiendee, ule chakula chako kwa kufurahi, kanywe mvinyo yako kwa kuwa na moyo mwema! Kwani kazi zako zilimpendeza Mungu tangu kale. Kavae nguo nyeupe siku zote, nacho kichwa chako kisikose mafuta! Kazifurahie siku za kuwapo pamoja na mkeo, umpendaye, siku zote za maisha yako zilizo za bure, Mungu alizokupa chini ya jua; kavifanye siku zako zote zilizo za bure! Kwani haya ndiyo, unayojipatia huku nchini kwa masumbuko yako, unayoyasumbuka chini ya jua. Yote, mkono wako utakayoyaona ya kuyafanya kwa nguvu yako, yafanye! Kwani kuzimuni, unakokwenda wewe, hakuna matendo wala mawazo wala ujuzi wala werevu wa kweli. Nilipoyatazama tena yaliyoko chini ya jua, nikaona, ya kuwa sio wepesi washindao katika mashindano ya mbio, wala sio mafundi wa vita washindao vitani, wala sio werevu wa kweli wapatao vilaji, wala sio watambuzi wapatao mali, wala sio wajuzi wapendezao, kwani wao wote kila mmoja wao huwa na siku zake na mambo yake yatakayompata. Mtu hazijui siku zake zimfaazo, huwa kama samaki wanaokamatwa katika wavu mbaya au kama videge wanaonaswa tanzini; vivyo hivyo nao wana wa Adamu hunaswa, siku zao zikiwa mbaya, nayo mabaya yakiwaangukia na kuwastusha. Nilipoutazama tena werevu wa kweli ulioko chini ya jua, nikauona kuwa mkubwa. Kulikuwa na mji mdogo, nao waume waliomo walikuwa wachache; kisha mfalme akaujia, akauzinga, akaujengea maboma makubwa. Basi, mle mjini akaonekana maskini mwenye werevu wa kweli, akauponya ule mji kwa huo werevu wake uliokuwa wa kweli; lakini baadaye hakuwako mtu aliyemkumbuka huyo maskini. Nikasema: Werevu wa kweli hufaa kuliko nguvu, lakini werevu wa maskini, ijapo uwe wa kweli, hubezwa, nayo maneno yake hayasikilizwi. Maneno ya werevu wa kweli wakiyasikiliza na kutulia hufaa kuliko makelele, mtawalaji anayoyapiga kwa wajinga. Werevu wa kweli hufaa kuliko vyombo vya vita, naye mkosaji mmoja huangamiza mema mengi. Mainzi waliokufa huyaozesha kwa kuyachafua mafuta ya mtengeneza manukato, ujinga hufanya makuu kuliko werevu wa kweli na utukufu. Moyo wa mwerevu wa kweli huelekea kuumeni, lakini moyo wa mjinga huelekea kushotoni. Napo njiani po pote, mjinga anapokwenda, hupotelewa na akili, hivyo hujitokeza kwao wote kuwa mjinga. Roho ya mtawalaji ikikuinukia, usiondoke mahali pako, kwani upole hutuliza makosa makubwa. Yako mabaya, niliyoyaona chini ya jua, ni kama kosa litokalo kwake mwenye ukuu: ni mjinga akitukuzwa sana, nao wenye mali wakikaa na kunyenyekezwa. Nikaona nao watumishi wanaopanda farasi, wakuu wakienda na kukanyaga nchi kama watumishi. Achimbaye mwina hutumbukia humo, naye abomoaye boma huumwa na nyoka. Avunjaye mawe huumizwa nayo, naye achanjaye kuni hujiponza papo hapo. Chuma kikiwa kimedugika, naye mwenyewe hakinoi, kipate makali, hana budi kutumia nguvu zaidi; hapo napo werevu wa kweli hufaa kwa kufanikiwa. Nyoka akiuma mtu, akiwa hajatabanwa, bado, basi, mwenye kutabana hanacho, anachokipata. Maneno ya kinywa chake mwerevu wa kweli hupendeza, lakini midomo ya mjinga hummeza. Mwanzo wa maneno ya kinywa chake ni ujinga, nao mwisho ni kusema upuzi mbaya. Yeye mjinga husema mengi; lakini hakuna mtu ayajuaye yatakayokuwa, tena yuko nani awezaye kumweleza yatakayokuwa nyuma yake? Masumbuko, anayoyasumbuka mjinga, humchokesha, kwa kuwa hajui hata njia ya kwenda mjini. Utaona mabaya, wewe nchi, mfalme wako akiwa kijana, nao wakuu wako wakila na mapema. Utaona mema, wewe nchi, mfalme wako akiwa mwana wa watu wenye macheo, nao wakuu wako wakila hapo panapopasa, wapate nguvu za kiume, wasile kwa kujilewesha. Kwa ajili yao wajengao kwa uvivu kipaa huinama, kwa ulegevu wa mikono nyumba huvuja. Watu hufanya karamu, wapate kucheka, nayo mvinyo huwafurahisha walioko huku nchini, nazo fedha hupata yote. Mfalme usimtukane hata kwa mawazo yako! Wala chumbani mwako, unamolala, usimtukane mwenye mali! Kwani ndege wa angani watayapeleka, uliyoyasema, naye mwenye mabawa atayatangaza hayo maneno. Mali zinazokutunza zitume kwenda ng'ambo ya bahari! Siku zitakapopita nyingi, utaziona tena. Nyingine uzigawie watu saba au wanane, kwani huyajui mabaya yatakayokuwa katika nchi. Mawingu yakijaa mvua huimiminia nchi. Tena mti ukiangukia upande wa kusini au wa kaskazini, basi, mahali papo hapo, mti ulipoangukia, ndipo, utakapokuwa. Auangaliaye upepo hatamwaga mbegu, wala ayatazamaye mawingu hatavuna. Kama asivyopatikana mtu anayeijua njia ya upepo, wala jinsi mifupa inavyotengenezeka kuwa mtoto tumboni mwake mwenye mimba, vivyo hivyo nawe huyajui matendo ya Mungu, anayoyatenda yote. Asubuhi zimwage mbegu zako, tena jioni usiulegeze mkono! Kwani hujui, kama ni hizi au ni zile zitakazofaa, au kama zote mbili pamoja zitazaa vema. Kweli mwanga ni mtamu, nako kuliona jua hupendeza macho. Kama mtu anapata miaka mingi ya kuishi, na aifurahie yote akizikumbuka siku za giza zitakazokuwa nyingi nazo; yote yatakayofuata ni ya bure. Wewe kijana, ufurahie utoto wako, moyo wako ule mema siku za ujana wako! Kazishike njia, moyo wako uzitakazo, kayafuate, macho yako yanayoyatazamia! Lakini ujue, ya kuwa hayo yote Mungu atakutakia shauri. Jiepushe penye masikitiko, yasiingie moyoni mwako, nayo mabaya yaangalie, yaupitie mwili wako mbali! Kwani utoto na ujana ni wa bure. Mkumbuke Muumbaji wako ukingali kijana bado, siku mbaya zikiwa hazijafika, wala miaka haijakupata bado, unayoisema: Hii sipendezwi nayo! Jua na mchana na mwezi na nyota zikiwa hazijaguiwa bado na giza, mawingu mengine yakitokea, mvua ikiisha kupita: siku hizo walinda nyumba watatetemeka, nao waume wenye nguvu watapindika, nao wanawake wasagao watakomesha kazi kwa kuwa wachache, nao wake waliochungulia madirishani wataguiwa na giza. Nayo milango ielekeayo njiani itafungwa, nacho kishindo cha mawe ya kusagia kitakuwa kidogo; ndipo, watu watakapoamka, jogoo akiwika, nao waimbaji wote wa kike watazipunguza sauti zao. Ndipo, watu watakapoogopa kupanda juu, nako njiani wataona mastusho; ni siku zile, mlozi unapochanua maua, mapanzi wasipoweza kuruka kwa kushiba, nacho kiungo cha pilipili kisipofaa kitu; kwani hapo mtu huiendea nyumba yake, atakamokaa kale na kale, nao waombolezaji humjia mara kwa mara. Kwani siku ziko karibu, kamba ya fedha itakapokatika, chano cha dhahabu kitakapopondeka, mtungi utakapovunjika kisimani, gurudumu la kutekea maji litakapokatika na kuangukia mlemle shimoni. Ndipo, nalo vumbi litakaporudi mchangani, lilikokuwa, nayo roho itarudi kwake Mungu aliyeitoa. Mpiga mbiu asema: Yote ni ya bure kabisa, yote pia ni ya bure. Jingine ni hili: huyu mpiga mbiu hakuwa mwerevu wa kweli yeye tu, ila nao watu aliwafundisha ujuzi, akawa mwenye mawazo makuu ya kuchunguza mambo, akatunga mafumbo mengi. Yeye mpiga mbiu alitafuta, aone maneno yapendezayo; nayo maneno yaliyokuwa ya kweli, yaliyoongoka, yakaandikwa. Maneno ya werevu wa kweli ni kama fimbo za wachungaji au kama misumari iliyopigiliwa vema; wenye kuyakusanya waliyapata kwa mchungaji mmoja. Jingine lililoko ni hili: onyeka, mwanangu, usijitie katika kazi hiyo! Kutengeneza vitabu ni kwingi mno, hakukomi, nako kujifunza mengi huchokesha mwili. Na tusikie neno linaloyachanganya yote: Mche Mungu na kuyaangalia maagizo yake! Kwani hivi ndivyo vinavyompasa kila mtu. Kwani matendo yote Mungu atayatakia shauri, nayo yaliyofichwa, kama ni mema, au kama ni mabaya. Na aninonee kwa manoneo ya kinywa chake! Kwani upendo wako hupendeza kuliko mvinyo. Mafuta yako ya kupaka hunukia vema, jina lako ni mafuta yaliyomiminwa, kwa hiyo wanawali hukupenda. Nivute, nikufuate nyuma! Na tupige mbio! Hata mfalme akiniingiza vijumbani mwake, na tupige vigelegele kwa kukufurahia wewe! Huo upendo wako tuutukuze kuliko mvinyo! Wanakupenda kwelikweli. Mimi ni mweusi, lakini ninapendeza, ninyi wanawake wa Yerusalemu! Nafanana na mahema ya Kedari, tena na mazulia ya Salomo. Msinionee kwa kuwa mweusimweusi! Ni jua lililonichoma. Wana wa mama yangu walinikasirikia, maana waliniweka kuwa mlinzi wa mashamba ya mizabibu, lakini hata shamba langu la mizabibu sikulilinda. Niambie wewe, mpendwa wa roho yangu: Unalishia wapi? Tena ni wapi, unapowapumzishia kondoo, jua likiwa kali? Mbona niwe kama mwenye kutangatanga penye makundi ya wenzako? “Usipopajua mwenyewe uliye mzuri kuliko wanawake wengine, toka tu na kuzifuata nyayo za kondoo, kavichunge vitoto vyako vya mbuzi matuoni kwa wachungaji! Ninakufananisha wewe, mpenzi wangu, na farasi avutaye gari la Farao. Mashavu yako hupendeza kwa kili za nywele, nayo shingo yako yenye ushanga. Na tukutengenezee vikufu vya dhahabu vyenye vifungo vya fedha. Mfalme akiwa anakaa mezani pake, manukato yangu ya narada hutoa mnuko wao mzuri.” Mpendwa wangu ni kifuko cha manemane kikaacho katikati ya maziwa yangu. Mpendwa wangu ni kichala cha mhina kitokacho mizabibuni kwenye Engedi. Nikikutazama, mpenzi wangu, u mwanamke mzuri, “u mwanamke mzuri kweli mwenye macho kama ya hua.” Wewe nawe, mpendwa wangu, u kijana mzuri, unapendeza kweli. Malalo yetu ni majani mabichi. “Boriti za nyumba yetu ni miangati, mbau zetu za kuzifunika kuta ni mvinje.” Mimi ni ua la uwago wa Saroni, ni nyinyoro ya mabondeni. “Kama ua lilivyo katikati ya miiba, ndivyo, mpenzi wangu alivyo katikati ya wanawali.” Kama mchungwa ulivyo katikati ya miti ya msituni, ndivyo, mpendwa wangu alivyo katikati ya vijana. Kwa kumtunukia nilikaa kivulini kwake; tunda lake ni tamu sana, nikilila. Akaniingiza nyumbani, wanyweamo mvinyo, nayo bendera yake iliyokuwa juu yangu, ni upendo. Nitieni nguvu kwa maandazi ya zabibu, kaniinueni kwa machungwa! Kwani mimi ni mgonjwa kwa kupenda sana. Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, nao wa kuume unanikumbatia. “Nawaapisha ninyi, wanawake wa Yerusalemu, nikiwataja paa na kulungu wake walioko porini, msimwamshe, wala msimhangaishe yeye ninayempenda, ila mwacheni tu, mpaka atakapopendezwa mwenyewe!” Iko sauti ya mpendwa wangu, naisikia, anakuja akiruka milimani, akichezacheza vilimani. Mpendwa wangu anafanana na paa mume au na kijana wa kulungu. Mtazame! Yuko akisimama nyuma ya kitalu chetu, akichungulia madirishani, akaonekana penye vyuma vyao. Mpendwa wangu ananiita na kuniambia: “Inuka, mpenzi wangu mzuri, uje hapa! Kwani tazama! Kipupwe kimepita, mvua nayo ikakoma, ikaenda zake. Maua yanaonekana katika nchi, siku za kuimba zimetimia, sauti za hua zinasikilika katika nchi yetu. Mkuyu unaanza kuziivisha kuyu zake changa, nayo mizabibu inachanua maua yanukayo vema; inuka, mpenzi wangu mzuri, uje hapa! Hua yangu hapo ngomeni penye mwamba, ulijificha magengeni, nipe kuuona uso wako, nipe kuisikia nayo sauti yako! Kwani sauti yako ni tamu, nao uso wako unapendeza. Tukamatieni nyegere, nyegere wale wadogo! Maana huiharibu mizabibu, nayo mizabibu yetu inachanua.” Mpendwa wangu ni wangu, nami ni wake yeye alishaye penye nyinyoro. Mpaka jua la mchana lipunguke ukali, vivuli vikijiendea mbiombio, geuka, mpendwa wangu, uruke kama paa au kijana wa kulungu, milimani kwenye makorongo! Nilipolala usiku nilimtafuta yeye, roho yangu inayempenda; nilimtafuta, lakini sikumwona. Na niinuke, nizunguke mjini, roho yangu inayempenda nimtafute barabarani na viwanjani; nilimtafuta, lakini sikumwona. Walinzi wazungukao mjini waliponiona, nikawauliza: Mmemwona yeye, roho yangu inayempenda? Nilipokwisha kuwapita kwenda mbele kidogo, ndipo, nilipomwona yeye, roho yangu inayempenda. Nikamshika, nisimwachie tena, mpaka nikamwingiza nyumbani mwa mama yangu, chumbani mwake yeye aliyenizaa. “Nawaapisha ninyi, wanawake wa Yerusalemu, nikiwataja paa na kulungu wake walioko porini, msimwamshe, wala msimhangaishe yeye ninayempenda, ila mwacheni tu, mpaka atakapopendezwa wenyewe!” Ni nani huyo apandaye kutoka nyikani? Anafanana kuwa kama wingu la moshi lililo kama nguzo, ni manemane na uvumba aliyovukiziwa na mavumbi ya manukato yote ya mchuuzi yanukayo vizuri. Tazameni! Kiko kiti, ni cha kifalme cha Salomo! Wanguvu sitini wanakizunguka, ndio wanguvu wa Waisiraeli. Wao wote wanashika panga, ni mafundi wa vita, kila mmoja anao upanga wake kiunoni pake wa kukingia mastusho ya usiku. Kiti hicho mfalme Salomo alijitengenezea kwa miti ya Libanoni, miguu yake aliifanya kwa fedha, maegemeo ni ya dhahabu, pa kukalia ni nguo nyekundu za kifalme. Hapo kati yako marembo mazuri mno yaliyoshonwa na wanawake wa Yerusalemu ya kumpendeza mfalme. Tokeni, wanawake wa Yerusalemu, mmtazame mfalme Salomo! Amevika kilemba, mama yake alichomfunga siku ya ndoa yake, maana ndiyo siku, moyo wake uliyoifurahia. Nikikutazama, mpenzi wangu, u mwanamke mzuri, nikikutazama, u mwanamke mzuri kweli, macho yako huwa ya hua yakichungulia katika mtandio wako; nywele zako zinafanana na kundi la mbuzi walalao upande wa kushukia wa mlimani kwa Gileadi. Meno yako ni kama kundi la kondoo waliokatwa manyoya, wanaopanda na kutoka majini wakiisha kuogeshwa, wote pia ni wenye wana wa pacha, kwao hakuna hata mmoja aliye peke yake. Midomo yake ni kama uzi wenye rangi nyekundu, kinywa chako kinapendeza nacho. Shavu lako huonekana mtandioni mwako kuwa kama komamanga ipevukayo sana. Shingo yako ni kama mnara wa Dawidi uliojengewa selaha, vigao elfu viko vimeangikwa kwake, vyote pia ni vya kuwakingia mafundi wa vita. Maziwa yako mawili yanafanana na vitoto viwili vya kulungu au na wana wa pacha wa paa walishwao penye nyinyoro. Mpaka jua la mchana lipunguke ukali, vivuli vijiendee mbiombio, ndipo, nitakapokwenda zangu mlimani kwenye manemane, hata kilimani kwenye uvumba. Wewe, mpenzi wangu, u mzuri peke yako, huna doadoa kabisa.” Toka Libanoni, mchumba wangu, twende pamoja! Toka Libanoni, twende pamoja, njoo! Tazama, huko juu Amana nako juu Seniri na Hermoni ndiko, simba wanakokaa, hata machui wako kule milimani. Umenipokonya moyo wangu, uliye umbu na mchumba wangu; umenipokonya moyo wangu, kwa kunitazama na jicho lako moja tu, ukanifunga kwa kikufu kimoja, unachokivaa shingoni pako. Ni kuzuri mno kukumbatiana na wewe, uliye umbu langu na mchumba wangu; kukumbatiana na wewe kunapendeza kuliko kunywa mvinyo, mnuko wa mafuta yako ni mzuri kuliko wa manukato yote. Midomo yako, mchumba wangu, inadondoka asali safi, asali na maziwa ndiyo yaliyoko chini ya ulimi wako, nao mnuko wa mavazi yako ni mzuri kama wa Libanoni. Umbu langu aliye mchumba wangu ni bustani iliyofungwa, ni kisima kilichofungwa, ni chemchemi iliyozibwa na kutiwa muhuri. Machipukizi yako ni kimwitu cha mikomamanga izaayo matunda yapendezayo sana, nayo mihina na miafu iko. Iko hata mianjano na mikumbi na mikoroshi na midalasini, miti yote itokayo uvumba na manemane nayo mishubiri iko, tena iko miti yote itokayo manukato yapitayo mengine. Nayo chemchemi iko bustanini na kisima chenye maji ya uzima na vijito vitokavyo Libanoni.” Inuka, upepo wa kaskazini! Njoo, upepo wa kusini! Vuma bustanini mwangu, minuko yake mizuri ifurikie! Mpendwa wangu aingie bustanini pake, ayale matunda yake yapendezayo! “Ninaingia bustanini pangu, umbu langu na mchumba wangu, niunge manemane na manukato yangu, nile masega yangu pamoja na asali yangu, ninywe mvinyo yangu na maziwa yangu. Nanyi wenzangu, leni, nyweni, mpaka mleweshwe na upendo! Nililala usingizi, lakini moyo ulikuwa macho; mara nikasikia, mpendwa wangu akigonga mlango: “Nifungulie, umbu langu, mpenzi wangu, hua yangu, mwenzangu atakataye! Kwa kuwa nimejazwa umande kichwani pangu, kwa kuwa misuko ya nywele zangu imejaa unyevu wa usiku.” Nikajibu: Nimekwisha kuivua kanzu yangu, nitaivaaje tena? Nikaisha kuiogesha miguu yangu, nitawezaje kuichafua tena? Ndipo, mpendwa wangu alipoutia mkono wake tunduni, moyo wangu ukarukaruka ndani kwa ajili yake. Nikainuka kumfungulia yeye mpendwa wangu, manemane yalipokuwa yanachuruzika mikononi pangu, navyo vidole vyangu vikadondokea manemane hapo pa kulishikia komeo. Lakini nilipokwisha kumfungulia mpendwa wangu, alikuwa ametoweka kabisa, yeye mpendwa wangu. Hapo aliposema, roho yangu ilitaka kuzimia, kwa hiyo nikamtafuta, lakini sikumwona, nikamwita, lakini hakunijibu. Walinzi wazungukao mjini waliponiona wakanipiga na kuniumiza, wakanivua mtandio wangu wale walinzi wa boma. Nawaapisha ninyi, wanawake wa Yerusalemu: Mkimwona mpendwa wangu mtampasha habari gani? Ya kuwa mimi nimeugua kwa upendo tu! “Mpendwa wako anawapitaje wapendwa wengine, wewe uliye mzuri miongoni mwa wanawake? Mpendwa wako anawapitaje wapendwa wengine, ukituapisha hivyo?” Mpendwa wangu ni mweupe sana, tena mwekundu, anajulikana katika elfu kumi. Mkikitazama kichwa chake, ni kama dhahabu tupu, misuko ya nywele zake nayo ni makuti yaning'iniayo, nazo ni nyeusi kama kunguru. Macho yake kama ya hua waliopo penye vijito vya maji, hujiogesha katika maziwa, huwapo na kuchangamka sana. Mashavu yake ni kama matuta yaliyopandwa manukato, namo juu mna vijanijani vinukavyo vizuri; midomo yake ni nyinyoro zidondokazo manemane ya majimaji. Mikono yake ni vigogo vya dhahabu zilizotiwa vito vingi vya Tarsisi, tumbo lake ni urembo wa meno ya tembo uliofunikwa na vito vya safiro. Paja zake ni nguzo za mawe meupe juu ya misingi ya dhahabu tupu; ukimtazama, anafanana na Libanoni, ni mtukufu kama miangati. Kinywa chake husema matamu tu, yaliyo yake yote pia hupendeza. Ndivyo mpendwa wangu alivyo, ndivyo, mwenzangu alivyo, ninyi wanawake wa Yerusalemu. “Je? Ndiko wapi, mpendwa wako alikokwenda, wewe uliye mzuri miongoni mwa wanawake? Ameshika njia gani mpendwa wako, tumtafute pamoja na wewe?” Mpendwa wangu ameshuka kwenda bustanini pake, kutembea bustanini penye matuta ya manukato, apate kuchuma nyinyoro. Mimi ni wake mpendwa wangu, naye mpendwa wangu ni wangu mimi; hulisha penye nyinyoro. “Kweli u mzuri kama Tirsa, unapendeza kama Yerusalemu, tena unaogopesha, mpenzi wangu, kama vikosi vyenye bendera. Yageuze macho yako, yasinitazame, kwani hunitatanisha; nywele zako zinafanana na kundi la mbuzi walalao upande wa kushukia wa milimani kwa Gileadi. Meno yako ni kama kundi la kondoo wanaotoka kuogeshwa, wote pia ni wenye wana wa pacha, kwao hakuna hata mmoja aliye peke yake. Shavu lako huonekana mtandioni mwako kuwa kama komamanga ipevukayo sana. Wako wanawake wa kifalme sitini na masuria themanini, tena wako wanawali wasiohesabika. Lakini yuko mmoja tu aliye hua wangu na mwenzangu atakataye, ni mwana wa pekee wa mama yake, aliyemzaa humpenda sana; wanawali wenzake wakimwona humwazia kuwa mwenye shangwe, nao wanawake wa kifalme na masuria humtukuza.” “Nani huyu mwanamke aonekaye kama mapambuzuko? Ni mzuri kama mwezi, anang'aa kama jua, anaogopesha kama vikosi vilivo vyenye bendera.” Nilishuka kwenda bustanini penye milozi, nijifurahishe kwa kuyaona machipukizi mapya yaliyoko bondeni; tena nilitaka kuitazama mizabibu, kama imechanua, nayo mikomamanga, kama imepata maua. Nilipokuwa siviangalii, roho yangu ikanipeleka, ikaniweka penye magari, nayo yalikuwa ya wakuu wa kwetu. “Rudi! Rudi, Sulamiti! Rudi! Rudi, tukutazame vema!” Mnatakaje kumtazama Sulamiti? Anafanana na michezo ya vita ya Mahanaimu? Miguu yako yenye mitalawanda ni mizuri mno, binti mkuu! Viuno vyako vinaviringana kama mapambo ya shingoni yaliyotengenezwa na mikono ya mtu aliye fundi kweli. Kitovu chako ni kama chano kilichoviringana, kisichokosa mvinyo iliyotiwa viungo vizuri; tumbo lako ni kama chungu ya ngano iliyozingwa na nyinyoro. Maziwa yako mawili hufanana na vitoto viwili vya kulungu, au na wana wa pacha wa paa. Shingo yako ni kama mnara wa meno ya tembo, macho yako ni kama viziwa vya kuko Hesiboni, vilivyoko hapo langoni, papitapo watu wengi, pua yako ni kama mnara wa Libanoni uelekeao Damasko. Kichwa chako hapa juu ni kama Karmeli, nywele za kichwani pako ni nyekundu kama nguo za kifalme, hata mfalme angependa kufungwa nayo hiyo misuko ya nywele. U mzuri peke yako kwa kupendeza sana, mpenzi wangu, unazidisha mambo yafurahishayo. Hivyo, ulivyokua, unafanana na mtende, nayo maziwa yako yanafanana na vichala vya mzabibu. Nilisema: Nitaupanda mtende huu, niyashike makuti yake, maziwa yako yaniwie kama vichala vya mzabibu, nao mnuko wa pumzi yako uniwie kama wa machungwa. Kinywa chako ni kama mvinyo njema inayompendeza mpendwa wako, akiinywa, nayo hupita polepole midomoni mwao walalao usingizi.” Mimi ni wake, mpendwa wangu, naye ananitunukia. Njoo, mpendwa wangu, tutoke kwenda shambani, tulale vijijini! Na tuondoke mapema kwenda mizabibuni, tutazame, kama mizabibu inachanua na kuyafunua maua. tutazama nayo mikomamanga, kama imepata maua! Hapo ndipo, nitakapokupa kukumbatiana na mimi. Mitunguja sasa inanuka, napo milangoni petu yapo matunda mazuri, mapya na ya mwaka uliopita; ndiyo, niliyokuwekea, mpendwa wangu. Laiti ungekuwa kama umbu aliyeyanyonya maziwa ya mama yangu! Kama ningekukuta nje ningekunonea pasipo kuona watu watakaonibeza. Ningekuongoza, nikupeleke nyumbani mwa mama yangu, ungenifundisha; kisha ningekunywesha mvinyo yenye viungo, nayo ni mbichi iliyotengenezwa kwa komamanga zangu. Mkono wake wa kushoto ungekuwa chini ya kichwa changu, nao wa kuume ungenikumbatia. Nawaapisha ninyi, wanawake wa Yerusalemu, msimwamshe, wala msimhangaishe yeye, ninayempenda, ila mwacheni tu, mpaka atakapopendezwa mwenyewe. “Ni nani huyu mke apandaye kutoka nyikani akimwegemea mpendwa wake?” “Chini ya mchungwa nilikuamsha; ndipo, mama yako aliposhikwa na uchungu alipokuzaa na kuona uchungu. Na uniweke moyoni mwako kama pete yenye muhuri! Na uniweke napo mkononi pako kama pete yenye muhuri! Kwani upendo ni wenye nguvu kama kifo, hushupaa kama kuzimu kwa wivu, miali yake ni miali ya moto, ni moto uwakao kwa kuwashwa na Bwana. Maji mengi hayawezi kuuzima upendo, majito makuu hayautosi, Kama mtu angezitoa mali zote zilizomo nyumbani mwake kwa kwamba: apate kupendwa, watu wangemsimanga kabisa.” Tumepata ndugu wa kike mdogo, naye maziwa yake hayako bado; sasa huyu ndugu yetu wa kike tumfanyie nini siku atakapoposwa? “Tutajenga juu yake kingio la fedha, kama yeye ni ukuta, lakini kama ni mlango tutaufunga kwa mbao za miangati.” Mimi ni ukuta, nayo maziwa yangu ni kama minara. Kwa hiyo nikawa machoni pake mahali patokeapo utulivu. Salomo alikuwa na shamba la mizabibu huko Baali-Hamoni, naye akawakodisha walinzi hilo shamba la mizabibu, kila mtu amtolee fedha elfu kwa matunda yake. Shamba langu la mizabibu ni langu, ninaliangalia mimi; zile fedha ninakuachia wewe, Salomo, tena mia mbili za kuwapa wao wayalindao matunda yake. “Wewe ukaaye bustanini, wenzako huisikiliza sauti yako; itoe namo masikioni mwangu mimi!” Kimbia, mpendwa wangu, kama paa au kijana wa kulungu warukao milimani kwenye manukato! Haya ndiyo maono ya Yesaya, mwana wa Amosi, aliyoyaona kwa ajili ya Yuda na kwa ajili ya Yerusalemu siku za Uzia na za Yotamu na za Ahazi na za Hizikia, waliokuwa wafalme wa Yuda. Sikilizeni, ninyi mbingu! Angalieni, ninyi nchi! Kwani Bwana anasema: Nilikuza wana, nikawapa utukufu; lakini wao wamenitengua. Ng'ombe humjua bwana wake. naye punda hupajua, mabwana wake wanapomwekea chakula; lakini Isiraeli hanijui, walio ukoo wangu hawanitambui. Utaona, wewe kabila lenye makosa, nanyi mnaolemewa na manza, mlizozikora, wewe kizazi cha wabaya, nanyi wana wapotovu! Wamemwacha Bwana na kumbeza Mtakatifu wa Isiraeli, wakarudi nyuma. Mnapigiwa nini, kwa kuwa mnafuliza bado kurudi nyuma? Kila kichwa kiko na vidonda, kila moyo umeugua. Toka wayo wa mguu mpaka kichwani hapana palipo pazima, ni madonda na machubuko na mapigo matupu; hayaoshwi, wala hayakufungwa, wala hayakulegezwa na mafuta. Nchi yenu ni mapori tu, miji yenu imeteketezwa na moto, mashamba yenu yanaliwa na wageni machoni penu; kweli ni mapori tu, kama nchi zilivyo zikiharibiwa na wageni. Paliposalia ni penye binti Sioni, ni kama kilindo mizabibuni, ni kama dungu shambani kwa miboga, kweli ni kama mji uliozungukwa na adui. Bwana Mwenye vikosi kama asingalitusazia hao wachache waliookoka, tungalikuwa kama Sodomu, tungalifanana na Gomora. Lisikilizeni neno lake Bwana, ninyi waamuzi wa Sodomu! Yaangalieni maonyo yake Mungu wetu, ninyi watu wa Gomora! Bwana anasema: Ni vya nini vipaji vyenu vingi, mnavyonitolea vya tambiko? Nimeshiba kondoo, mlionichomea, hata mafuta ya ndama wanonao, damu zao ng'ombe na wana kondoo na mbuzi hazinipendezi. Mnapokuja kuoneka machoni pangu, ni nani aliyevitaka hivyo mikononi mwenu, mkija kuzikanyaga nyua zangu? Acheni kuleta tena vilaji vya tambiko visivyofaa! Uvumba nao hunitapisha, hata sikukuu za miandamo ya mwezi nazo za mapumziko na za makusanyiko; sivumilii, upotovu ukiwa hapohapo, mnaponikusanyikia. Roho yangu huzichukia sikukuu zenu za miandamo ya mwezi nazo sikukuu zenu nyingine, zimeniwia mzigo mzito, nimechoka kuuchukua tena. Mkininyoshea mikono yenu, nitayafumba macho yangu, yasiione, hata mkikaza kuniomba, sisikii; maana mikono yenu imejaa damu. Iosheni na kuitakasa! Uondoeni ubaya wa matendo yenu, macho yangu yasiuone tena! Msiendelee na kufanya mabaya! Jifundisheni kufanya mema! Tafuteni njia ya kunyosha maamuzi mkiwapingia wakorofi! Waamulieni wafiwao na wazazi! Wagombeeni wajane! Njoni, tuumbuane! Ndivyo, asemavyo Bwana. Makosa yenu ijapo yawe mekundu kama damu, yatakuwa meupe kama chokaa juani; ijapo yawe mekundu kama nguo za kifalme, yatakuwa kama pamba. Ikiwapendeza, mnisikie, basi, mtakula mema ya nchi. lakini mkikataa, mkaacha kutii, mtaliwa na panga. Kwani kinywa chake Bwana kimesema. Kumbe mji uliokuwa wenye welekevu umegeuka kuwa wenye ugoni! Ulikuwa umejaa maamuzi yanyokayo, wongofu ukapata kao kwako, lakini sasa ni kao la wauaji. Fedha yako imegeuka kuwa mavi ya chuma tu, mvinyo yako imechanganywa na maji. Wakuu wako hufanya fujo, wenzao ni wezi, wao wote hupenda matunzo, hufuata fedha za kupenyezewa, wafiwao na wazazi hawawaamulii, wala mashauri ya wajane hayafiki kwao. Kwa sababu hiyo ndivyo, asemavyo Bwana, yeye Bwana Mwenye vikosi amtawalaye Isiraeli: Patafika, nitakapojituliza kwao wapingani wangu, nikiwalipiza adui zangu! Ndipo, mkono wangu utakapokurudia tena, hapo nitayayeyusha mavi yako ya chuma kwa dawa kali, niyaondoe yasiyokupasa yote yaliyomo. Kisha nitakupa tena waamuzi kama huko kale, nao wakata mashauri watakuwa kama wao wa mwanzoni. Kwa hiyo utaitwa Ngome ya Wongofu au Mji wenye Welekevu. Sioni utakombolewa kwa maamuzi ya kweli, nao watu wake walioigeuza mioyo watakombolewa kwa wongofu. Lakini wapotovu na wakosaji watavunjwa wote pamoja, nao waliomwacha Bwana watatoweka. Kwani watatwezwa kwa ajili ya mitamba, mliyoitunukia, nazo nyuso zenu zitaiva kwa kuona soni kwa ajili ya mashamba, mliyoyachagua. Kwani mtakuwa kama mtamba uliokauka pamoja na majani yake, au mtafanana na shamba lisilo na maji. Mwenye nguvu atageuka kuwa kama madifu makavu, nazo kazi zake zitakuwa kama cheche la moto; kisha yatateketea yote pamoja, asipatikane awezaye kuuzima moto huo. Hili ni neno, Yesaya, mwana wa Amosi, aliloliona la Yuda na la Yerusalemu: *Mwisho wa siku utakapotimia, mlima wenye Nyumba ya Bwana utakuwa umeshikizwa na nguvu, uwe wa kwanza wa milima, uende juu kuliko vilima vingine, hata wamizimu wote wataukimbilia. Makabila mengi ya watu watakwenda wakisema: Njoni, tupande mlimani kwa Bwana kwenye Nyumba ya Mungu wa Yakobo! Atufundishe, njia zake zilivyo, tupate kwenda na kuifuata mikondo yake! Kwani ufundisho utatoka Sioni, namo Yerusalemu litatoka Neno la Bwana. Ndipo, atakapowaamulia wamizimu na kuyapatiliza makabila mengi ya watu; nao watazifua panga zao kuwa majembe, hata mikuki yao kuwa miundu, kwani halitakuwako tena kabila litakalochomolea jingine upanga, wala hawatajifundisha tena mapigano ya vita. Mlio wa mlango wa Yakobo, njoni, tuendelee pamoja katika mwanga wa Bwana!* Kwani umewatupa wao waliokuwa ukoo wako, wale wa mlango wa Yakobo, kwani wamejaa mambo yatokayo maawioni kwa jua, huagulia mawingu kama Wafilisti, hufanya maagano nao vijana wa nchi ngeni. Nchi yao ikajaa fedha na dhahabu, malimbuko yao hayana mwisho; nchi yao ikajaa farasi, magari yao hayana mwisho. Nchi yao ikajazwa vinyago; huziangukia kazi za mikono yao, walizozitengeneza kwa vidole vyao. Watu wakavinyenyekea, mabwana nao wakaviinamia; hivi hatawaondolea kabisa. Nenda magengeni! Jifiche uvumbini! Usiuone uso wake ukutishao wala utukufu wa ukuu wake! Macho ya watu wajivunao yatanyenyekezwa, nao waume wajikwezao watainamishwa, kwa maana atakayetukuka siku ile ni Bwana peke yake. Kwani siku ya Bwana Mwenye vikosi itawajia watu, wanyenyekezwe wenye majivuno na ukuu, nao wajitukuzao; nayo miangati ya Libanoni iliyo mikubwa na mirefu, nayo mikwaju yote ya Basani inyenyekezwe, nayo milima mirefu yote, hata vilima vyote vinavyokwenda juu sana; nayo minara mirefu yote, hata maboma yote yenye nguvu; nazo merikebu zote za Tarsisi ziletazo mali na vitu vizuri vyote pia, watu wanavyovitamani. Nao watu wajivunao watainamishwa, hata waume wajikwezao watanyenyekezwa, kwa maana atakayetukuka siku ile ni Bwana peke yake, navyo vinyago vitatoweka vyote pia. Ndipo, watakapokwenda mapangoni kwenye magenge namo mashimoni kwenye nchi kavu, wasiuone uso wa Bwana uwatishao wala utukufu wa ukuu wake, atakapoinuka kuistusha nchi. Siku ile watu watavikupa vinyago vyao, ijapo viwe vya fedha na vya dhahabu; hivyo, walivyojifanyizia vya kuvitambikia, watavitupa kwenye panya na mapopo, wapate kujiendea kwenye nyufa za magenge na kwenye mapango ya miamba, wasiuone uso wa Bwana uwatishao wala utukufu wa ukuu wake, atakapoinuka kuistusha nchi. Sasa waacheni wale watu! Nao puani mwao ni pumzi tu; huwaziwa kuwa nini? Mtaona, Bwana aliye Bwana Mwenye vikosi akiondoa katika Yerusalemu na katika Yuda yote yatumikayo kuwa shikizo: kila shikizo la vilaji na kila shikizo la maji; wenye nguvu nao wajuao kazi za vita, waamuzi na wafumbuaji, waaguaji na wazee, wakuu wa askari na wenye macheo makubwa, wakata mashauri na mafundi wa kazi na mafundi wa uganga. Kisha nitawapa vijana, wawe wakuu wao, nao wenye ukorofi watawatawala; nao wenyewe watatesana waume na waume wenzao, kila mtu na ndugu yake, vijana watajivuna na kuwabeza wazee, nao wanyonge watawabeza wenye utukufu. Hapo itakuwa, mtu amkamate ndugu yake, ambaye alizaliwa naye nyumbani mwa baba yake, amwambie: Unazo nguo bado, sharti uwe mwamuzi wetu! Hame hili liwe mkononi mwako! Naye atajibu siku ileile na kupaza sauti: Mimi si mganga! Humu nyumbani mwangu hamna mkate wala nguo, msiniweke kuwa mwamuzi wenu! Kwani Yerusalemu utakuwa umejikwaa, nayo Yuda itakuwa imeanguka, kwa kuwa ndimi zao na kazi zao zilimpinga Bwana na kuyachafua macho yake yenye utukufu, ukorofi wa nyuso zao ukawaumbua, nao huyasimulia makosa yao pasipo kuyaficha kwa hivyo, wanavyofanana nao Wasodomu. Roho zao zitalipizwa vibaya, walivyojifanyizia wenyewe. Yawazeni, ya kuwa waongofu huona mema, kwani huyala mapato ya kazi zao! Lakini wasiomcha Mungu huona mabaya, kwani mikono yao iliyoyafanya, watafanyiziwa nao. Wanaowasonga walio ukoo wangu ni watoto, nao wanawake ndio wanaowatawala. Ninyi mlio ukoo wangu, viongozi wenu huwapoteza, nazo njia zenu zilizowapasa kuzishika huzifisha. Bwana ameinuka kupigana, Bwana amesimama kuyapatiliza makabila ya watu. Bwana atakuja kuwahukumu wazee na wakuu wao walio ukoo wake, kwamba: Ninyi mmeilisha mizabibu yangu! Mliyoyanyang'anya wanyonge, yamo nyumbani mwenu. Imekuwaje, mkiwaponda hivyo walio ukoo wangu? Mkizirarua nyuso za wanyonge hivyo? Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Mwenye vikosi. Bwana amesema: Kwa kuwa wanawake wa Sioni wamejikuza, wakatembea na kunyosha shingo na kutupia wengine macho yenye utongozi, wakienda na kuchezacheza na kuipigapiga mikufu ya miguu yao: Bwana atawauguza wanawali wa Sioni upele wa vichwani, yeye Bwana atawavua nazo nguo za kujifunika shungi. Siku ile Bwana atayaondoa mapambo kwao: vikuku na mifano ya jua vipajini nayo manyamwezi shingoni, mapete masikioni na mikufu mikononi na mabuibui nyusoni; hata miharuma vichwani na mikufu miguuni na mikanda viunoni na vichupa vya marashi vifuani na hirizi zote miilini po pote, nazo pete vidoleni na vipini puani, tena nguo za sikukuu, kama marinda na kanga na vijamanda, hata vioo na fulana za hariri na vilemba na kaya. Hivyo penye manukato mazuri utakuwa mnuko wa kuoza, penye mikanda watapata kamba tu, penye misuko ya nywele patakuwa na vipara, penye zile nguo za urembo watajivika magunia, maumbufu matupu yatapashika mahali pa uzuri. Waume wenu watauana kwa panga, vijana wenu wenye nguvu watamalizika vitani. Kwa hiyo malango yake yatapiga kite kwa kusikitika, nao wenyewe watakaa uvumbini kwa kuwa peke yao tu. Siku ile wake saba watamshika mume mmoja na kumwambia: Tutajipatia wenyewe vilaji na mavazi, tunataka tu kuitwa kwa jina lako, utuondolee soni zetu! Siku ile mche wa Bwana utakuwa wenye urembo na macheo, nao uzao wa nchi utakuwa wenye ukuu na utukufu kwao Waisiraeli waliopona. Atakayekuwa amebakizwa Sioni, naye atakayekuwa amesazwa Yerusalemu ataitwa mtakatifu, ni kila mmoja wao aliyeandikiwa kuwapo Yerusalemu. Hapo ndipo, Bwana atakapokuwa amekwisha kuyaosha machafu yao wanawali wa Sioni, napo ndipo, atakapokuwa amekwisha kuzitowesha mwao damu zilizomwagwa Yerusalemu; atavifanya kwa nguvu za roho yenye mapatilizo na kwa nguvu za roho yenye moto. Kwenye makao yote ya mlimani kwa Sioni nako kwenye makutano ya kumtambikia Bwana atakuumbia siku zote wingu litakalokuwa lenye moshi la mchana na lenye mwanga wa moto uwakao usiku, kwani chote chenye utukufu hupaswa na kifuniko chake. Hivyo watapata pa kukalia kivulini mchana, ukali wa jua usiwaumize, tena pa kukimbilia na pa kujifichia, kimbunga kisiwaangushe, wala mvua isiwapige. Na niimbe mambo ya mpendwa wangu! Ni wimbo wa mpenzi wangu wa kuiimbia mizabibu yake. Mpendwa wangu alikuwa na shamba la mizabibu penye kilima kilichoiotesha sana. Akalima na kuchimba, hata mawe akayaokota, akapanda mizabibu mizuri akajenga dungu katikati, akachimbua nalo kamulio kwake; kisha alingoja, izae zabibu, lakini ikazaa mbaya zisizolika. Sasa ninyi mkaao Yerusalemu nanyi waume wa Yuda, tuamulieni mimi na mizabibu yangu! Yako mambo gani ya kuifanyizia mizabibu, nisiyoifanyizia? Mbona nilikaa na kuzingojea zabibu, ikanizalia tu zisizolika? Sasa na niwajulishe, mimi nitakayoifanyizia mizabibu yangu: nitaliondoa boma lao, iwe malisho, nitakibomoa kitalu chao, ife kwa kukanyagwa. Nitaiacha, iwe pori lenyewe, isipogolewe wala isilimiwe, pakue mikunju na mibigili; kisha nitayaagiza mawingu, yasiinyeshee mvua. Kwani mizabibu ya Bwana Mwenye vikosi ni mlango wa Isiraeli na watu wa Yuda, ndio shamba lake lipendwalo naye. Akangojea manyofu, lakini alipotazama, ni mapotovu; akangojea wongofu, lakini alipotazama, ni vilio tu. Yatawapata wanaokusanya nyumba na nyumba ndio wanajiongezea mashamba na mashamba, pasiwepo tena mahali pasipo penu, mkae peke yenu katika nchi. Masikioni mwangu limo neno la Bwana Mwenye vikosi: Kweli nyumba nyingi zitakuwa mahame, ijapo ziwe kubwa na nzuri, asipatikane mtu wa kukaa humo. Kwani mashamba kumi ya mizabibu yatatoa kibuyu kimoja tu, kikapu kizima cha mbegu kitaleta pishi moja tu. Yatawapata waamkao mapema wakijitafutia vileo nao wakaao mpaka usiku kwenye pombe na kuvimbisha vichwa. Hapo wanyweapo yako mazeze na mapango, hata matoazi na mazomari, lakini kazi za Bwana hawazitazami, wala matendo ya mikono yake hawayaoni. Kwa hiyo wao walio ukoo wangu watatekwa wakiwa hawajui maana, watukufu wao watakuwa wenye njaa, nao walio watuwatu tu watazimia kwa kiu. Kwa hiyo kuzimu kutakuwa kumejipanua na kukifumbua kinywa chake pasipo mpaka, watukufu wa Sioni pamoja na watu wake wapate kushuka nao waliochezacheza mle na kupiga vigelegele vya furaha. Hapo watu watainamishwa, nao waume watanyenyekezwa, hayo macho yenye majivuno yatanyenyekezwa. Lakini Bwana Mwenye vikosi atatukuka kwa kunyosha maamuzi, yeye aliye Mungu mtakatifu atajulika kwa wongofu kuwa Mtakatifu kweli. Wana wa kondoo watalisha hapo, kama ni malisho yao, nako kwenye mahame ya wale wakwasi watakula wageni. Yatawapata wajivutiao mabaya kwa vigwe vya udanganyifu, tena makosa kwa kamba za magari. Ndio wanaosema: Na apige mbio, afanye upesi matendo yake, tuyaone! Shauri lake Mtakatifu wa Isiraeli na litimie na kutokea, tulitambue! Yatawapata wanaosema: Kibaya ni chema nacho chema wanakiita kibaya. Giza huigeuza kuwa mwanga, nao mwanga huugeuza kuwa giza. Machungu huyageuza kuwa matamu, nayo matamu huyageuza kuwa machungu. Yatawapata wanaojiwazia wenyewe kuwa werevu wa kweli na watambuzi. Yatawapata walio wenye nguvu za kunywa pombe, walio na ufundi wa kuchanganya vileo. Kwa kupenyezewa mali huwashindisha wapotovu shaurini, lakini wongofu wao waongokao huutengua, wasishinde! Kwa hiyo watakuwa hivyo: kama ndimi za moto zinavyokula mabua, au kama majani makavu yanavyojipinda motoni, ndivyo, mizizi yao itakavyobunguka, nayo maua yao yatapeperushwa kama mavumbi, kwani waliyakataa Maonyo yake Bwana Mwenye vikosi, wakalibeza Neno lake Mtakatifu wa Isiraeli! Kwa hiyo Bwana akawachafukia walio ukoo wake, mkono wake ukawainamia, ukawapiga; milima ikatetemeka, mizoga yao ikawa kama mataka njiani. Kwa hayo yote makali yake hayajatulia bado, mkono wake ungaliko umekunjuka bado. Atatweka bendera ya kuwaitia wamizimu wakaao mbali nao wakaao kwenye mapeo ya nchi atawapigia mbiu, na mwaone, wakija na kupiga mbio sana. Mwao hao hamna mchovu ajikwaaye mara kwa mara, wala hamna apendaye kusinzia wala kulala usingizi, wala hamna mwenye mshipi kiunoni ufungukao, wala hamna mwenye viatu vikatikavyo mikanda. Mishale yao itakuwa imenolewa, nyuta zao zitakuwa zimepindwa, kwato za farasi wao zitaonekana kuwa ngumu kama mawe, magurudumu ya magari yao yatapiga mbio kama upepo mkali. Mazomeo yao ni kama ngurumo ya simba, hulia kama wana wa simba. Watakuja na kuvuma na kukamata mateka, wayapeleke kwao; napo hapo hatakuwapo atakayewaponya. Makelele, watakayowapigia siku ile, yatakuwa kama maumuko ya mawimbi ya bahari; kama mtaichungulia nchi, itakuwa yenye giza la kuogopesha, mwanga utakuwa umegeuka giza kwa weusi wa mawingu yaliyoko juu yake. *Ule mwaka, mfalme Uzia alipokufa, nilimwona Bwana, akikalia kiti kirefu cha kifalme kilichowekwa juu, nazo nguo zake zikalijaza Jumba takatifu. Maserafi walikuwa wanasimama juu yake; kila mmoja wao alikuwa mwenye mabawa sita: mawili aliyatumia kuufunika uso wake, mawili kuifunika miguu yake, mawili ya kurukia. Wakapaliziana sauti kwamba: Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Bwana Mwenye vikosi! Nchi zote zimejaa utukufu wake! Ikatetemeka hata misingi ya vizingiti kwa ukuu wa sauti yake aliyeyatangaza; nayo nyumba ikajaa moshi. Nikasema: Ninakufa, ninaangamia! Kwani ndimi mtu mwenye midomo isiyotakata, tena mimi ninakaa kwa watu wenye midomo isiyotakata, kwani macho yangu yamemwona Mfalme, ndiye Bwana Mwenye vikosi! Hapo mmoja wao wale Maserafi akaruka, akanijia; namo mkononi mwake alishika kaa la moto, alilolichukua kwa koleo penye meza ya kutambikia. Akagusa nalo kinywa changu, akasema: Tazama! Hili lilipoigusa midomo yako, manza zako, ulizozikora, zimekutoka, nayo makosa yako yamefunikwa. Nikasikia sauti ya Bwana, akisema: Nitamtuma nani? Yuko nani atakayetuendea? Nikajibu: Mimi hapa! Nitume!* Akasema: Nenda, uwaambie watu wa ukoo huu kwamba: Kusikia mtasikia, lakini hamtajua maana; kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Kwani mioyo yao walio ukoo huu uishupaze, nayo masikio yao uyazibe, nayo macho yao uyafumbe, wasije wakaona kwa macho yao, au wakasikia kwa masikio yao, au wakajua maana kwa mioyo yao, wakanigeukia, nikawaponya! Nikasema: Mpaka lini, Bwana? Akasema: Mpaka hapo, miji itakapokuwa mahame, kwa kuwa hamna mwenye kukaa humo, kwa kuwa nyumba hazina watu; mpaka hapo, nchi nayo itakapoangamia kwa kuwa mapori tu; mpaka hapo, Bwana atakapowapeleka watu mbali, mahame yawe mengi katika nchi hii. Tena kama sao litakuwa fungu la kumi tu, litaangamizwa mara nyingine. Litakuwa kama mkwaju au mtamba: ukikatwa, kunasalia shina lake; hilo shina lake litakuwa mbegu takatifu. Siku za Ahazi, mwana wa Yotamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, ndipo, Resini, mfalme wa Ushami, na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Isiraeli, walipokuja kupiga vita nao waliomo Yersalemu, lakini hawakuweza kuwashinda vitani. Walio wa mlango wa Dawidi walipopashwa habari, ya kwamba vikosi vya Washami vimeingia katika nchi ya Efuraimu, vikapiga makambi, mioyo yao ikatikisika nayo mioyo ya watu wao, kama miti ya mwituni inavyotikiswa na upepo. Lakini Bwana akamwambia Yesaya: Toka wewe na mwanao Seari-Yasubu (Sao litarudi), uje kukutana na Ahazi, mwishoni pa mfereji wa maji ya ziwa la juu, kule barabarani panapokwenda kwenye shamba la Mfua nguo. Mwambie: Jiangalie, utulie, usiogope! Jipe moyo kwa ajili ya moshi wa hivyo vijinga viwili vilivyomo katika kuzimika, ijapo makali ya Resini na ya Washami na ya mwana wa Remalia yawakishe moto. Kweli Washami, Waefuraimu na mwana wa Remalia wamekulia njama mbaya ya kwamba: Na tupande kwenda Yuda, tuwastushe tukiwashambulia na kuwashinda, kisha tumweke mwana wa Tabeli kuwa mfalme kwao katikati! Kwa sababu hii Bwana Mungu anasema: Hayatatimia! Hayatakuwa! Kwani kichwa cha Ushami ni Damasko, nacho kichwa cha Damasko ni Resini, tena miaka 65 itakapopita, Efuraimu atakuwa amepondwa kabisa, wasiwe ukoo tena. Kichwa cha Efuraimu ni Samaria, nacho kichwa cha Samaria ni mwana wa Remalia. Ikiwa mnakosa wa kumtegemea, kweli hamtategemezwa. Bwana akaendelea, akamwambia Ahazi kwamba: Jiombee kielekezo kwake Bwana Mungu wako! Omba kilicho mbali kuzimuni au kilicho mbali mbinguni! Ahazi akajibu: Sinacho nitakachokiomba, nisimjaribu Bwana. Ndipo, (Yesaya) aliposema: Sikilizeni, ninyi mlio wa mlango wa Dawidi! Je? Havijawatoshea kuwachokoza watu, mkimchokoza naye Mungu wangu? Kwa hiyo Bwana atawapa mwenyewe kielekezo, ni hiki: Tazama, mwanamwali atapata mimba, atazaa mtoto mwanamume, nalo jina lake atamwita Imanueli (Mungu yuko nasi). Atakula maziwa yenye mafuta na asali, mpaka atakapojua kukataa mabaya na kuchagua mema. Yule kijana atakapokuwa hajajua bado kukataa mabaya na kuchagua mema, nchi ile itakuwa imeachwa, sasa unawastukiaje wafalme wake wawili? Bwana atawaletea ninyi, wewe nao wa ukoo wako nao wa mlango wa baba yako, siku zisizokuja bado kuanzia siku ile, Waefuraimu walipojitenga kwao Wayuda; itakuwa hapo, mfalme wa Asuri atakapokuja. Siku ile mbung'o walioko mwishoni kwenye mito ya Misri nao nyuki walioko katika nchi ya Asuri Bwana atawapigia miluzi, waje. Watakuja kutua wote pamoja katika mabonde na makorongo, katika nyufa za magenge, hata katika maboma yote ya miti yenye miiba na malishoni po pote. Siku ile Bwana atamtumia mfalme wa Asuri kuwa kama wembe uliokopwa ng'ambo ya lile jito kubwa, awanyoe nywele za vichwa na za miguu, hata za ndevu zitamalizwa zote pia. Siku ileile mtu atafuga king'ombe kimoja na vibuzi viwili tu. Lakini kwa kupata maziwa mengi kwao hao atakula mafuta; wote watakaosalia katika nchi hiyo watakula mafuta na asali. Tena siku ile kila mahali penye mizabibu elfu iletayo sasa fedha elfu patakuwa penye mikunju na mibigili. Watu wakienda mahali kama hapo watashika mishale na pindi, kwani nchi nzima itakuwa mapori yenye mikunju na mibigili. Nako kwenye milima kote kunakolimwa sasa na majembe, watu hawatakwenda tena huko kwa kuiogopa mikunju na mibigili, watakutumia tu kwa kuchungia ng'ombe na kondoo na mbuzi, wachezeechezee kuko huko. Bwana akaniambia: Jitwalie ubao mkubwa, kauandike kwa kalamu ya kimtu, watu waweze kuusoma: Teka upesi! Pokonya hima! Nami nitachukua mashahidi welekevu, wanishuhudie, ni mtambikaji Uria na Zakaria, mwana wa Yeberekia. Kisha nikafika kwake mfumbuaji wa kike; akapata mimba, akazaa mwana wa kiume. Bwana akaniambia: Ita jina lake Teka upesi! Pokonya hima! Kwani kijana atakapokuwa hajajua kuita: Baba! au: Mama! watu watakuwa wameyachukua mapato ya Damasko na mateka ya Samaria, wakiyapeleka machoni pake mfalme wa Asuri. Bwana akasema tena na mimi mara nyingine akiniambia: Kwa kuwa watu hawa wameyakataa maji ya Siloa yaendayo polepole, wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia, kwa sababu hii wataona, Bwana akiwaletea maji makali ya jito kubwa yaliyo mengi; kwani mfalme wa Asuri atakuja na utukufu wake wote. Hapo ndipo, vijito vyote vitakapopanda kwa kuwa na maji mengi, nayo yatapita kingo zao zote. Ataiingia nchi ya Yuda kwa nguvu, maji yatafika mpaka shingoni kwa kujaa na kufurika, nayo mabawa yake yakunjukayo yataieneza nchi yako, Imanueli, ijapo iwe pana. Kasirikeni, ninyi makabila ya watu, kalegeeni kwa kituko! Sikilizeni, nyote mkaao katika nchi za mbali! Jifungeni, kisha legeeni kwa kituko! Pigeni shauri, kisha livunjike! Semeni neno, kisha lisitimie! Kwa kuwa Imanueli yuko. Kwani hivi ndivyo, Bwana alivyoniambia aliponishika mkono na kunionya, nisiifuate njia ya watu wa ukoo huu, akisema: Msiite angamizo vyote, watu wa ukoo huu wanavyoviita angamizo! Wala msiyaogope, wanayoyaogopa, wala msiyastukie! Ila mtakaseni Bwana Mwenye vikosi! Yeye ndiye, mmwogope na kumstukia! Hivyo atakuwa mwenye kutakasa, tena atakuwa jiwe la kujigongea na mwamba wa kujikwalia kwao milango yote miwili ya Isiraeli; nao wakaao Yerusalemu atawawia kama mtego wa tanzi. Wengi watajikwalia papo hapo, waanguke, wachubuke; wengine watanaswa, watekwe. Yafunge, uliyoshuhudiwa! Kisha yatie muhuri pamoja na Maonyo machoni pao wanafunzi wangu! Basi, sasa nitakuwa ninamwegemea Bwana na kumngojea, maana amewaficha uso wake walio mlango wa Yakobo. Tazama, mimi pamoja na hawa watoto, Bwana alionipa, tunakuwa vielekezo na vioja kwao Waisiraeli; ndivyo, alivyotuwekea Bwana Mwenye vikosi akaaye mlimani kwa Sioni. Kama wanawaambia: Watafuteni wajuao kukweza mizimu nao wapunga pepo wanaonong'ona na kusema na sauti ndogo! wajibuni: Wasimtafute Mungu wao, wamwulize? Waulizeje wafu kwa ajili yao walio hai? Yarudieni Maonyo yaliyoshuhudiwa! Kweli wawezao kusema maneno kama yale hawajatokewa bado na mionzi ya jua. Hutangatanga katika nchi kwa kuumizwa na ukiwa na njaa; tena kwa kuumizwa na njaa huchafuka, amtukane mfalme wao na mungu wao na kutazama juu. Kisha hutazama chini tena kwa kusongeka na kukosa mwanga, kwani wamo katika giza, nalo linawaogopesha, kwani wamesukumwa kukaa katika usiku mweusi. Lakini huko kuliko na masongano kama hayo giza haitakaa kabisa. Siku za mbele nchi ya Zebuluni na nchi ya Nafutali alizitia soni, lakini huko nyuma atazipatia utukufu kwenye njia ya baharini na ng'ambo ya Yordani, Galilea ya wamizimu iliko. Watu waliofanya mwendo gizani wameona mwanga mkuu, waliokaa penye kivuli kiuacho mwanga umemulika juu yao. Wewe umekuza watu, wawe wengi, ukawapatia furaha kuu; wanakufurahia, kama watu wanavyofurahi penye mavuno, kama wanavyoshangilia wakigawanya mateka. Kwani umeivunja miti ya kuchukulia mizigo pamoja na magongo yaliyowapiga migongoni, nazo fimbo za wasimamizi, kama ulivyofanya siku ya kuwapatiliza Wamidiani. Kwani mata yote, waliyoyashika kwenye mapigano, nazo nguo zilizofuliwa katika damu zitateketezwa kwa ukali wa moto. *Kwani tumezaliwa mtoto, tumepewa mwana wa kiume, nao ufalme uko begani pake. Jina lake wanamwita: Ajabu la mizungu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa kale na kale, Mfalme wa utengemano. Ufalme wake ni mkubwa, nao utengemano hauna mwisho kwenye kiti cha Dawidi na katika nchi zote, azitawalazo; atazitengeneza na kuzishikiza akiziamua kwa wongofu kuanzia sasa na kuendelea vivyo hivyo kale na kale. Bwana Mwenye vikosi atajihimiza kuyafanya hayo.* Bwana alituma neno la kuwatisha wa Yakobo, linawapasa Waisiraeli nao. Watu wote watalitambua, kama Waefuraimu nao wakaao Samaria wasemao kwa majivuno na kwa mawazo makuu ya mioyo yao kwamba: Majengo ya matofali yalipoanguka, tutapajenga kwa mawe ya kuchonga; mitamba ilipokatwa, tutapanda miangati mahali pao. Kwa hiyo Bwana alipandisha kwao vikosi vya Resini, viwasonge, nao adui zao akawachochea, wawajie: upande wa mbele wakaja Waasuri upande wa nyuma Wafilisti, wakawala Waisiraeli na kuasama vinywa kabisa. Lakini kwa hayo yote makali yake hayajatulia bado, nao mkono wake ungaliko umekunjuka. Nao walio ukoo wake hawakurudi kwake aliyewapiga, Bwana Mwenye vikosi hawakumtafuta. Basi, siku moja Bwana alikata kwao Waisiraeli kichwa na mkia, hata makuti na majani. Kichwa ndio wazee na wenye macheo, mkia ndio wafumbuaji wafundishao mambo ya uwongo. Kwani viongozi wa ukoo huu walikuwa wapotevu, nao walioongozwa nao wakaangamizwa. Kwa sababu hii Bwana hakupendezwa na vijana wao, hakuwahurumia wala waliofiwa na wazazi wala wajane wao, kwani hao wote humbeza Mungu kwa kufanya mabaya, kila kinywa husema mapumbavu. Lakini kwa hayo yote makali yake hayajatulia bado, nao mkono wake ungaliko umekunjuka. Kwani kule kumbeza Mungu kuliendelea kama moto uwakao. unakula miiba na mibigili mikavu, unachoma vichaka vya msituni na kupandisha mawingu mazima ya moshi. Nchi ikateketea kwa moto wa makali ya Bwana Mwenye vikosi, watu wakawa kama chakula cha moto, kwa hiyo hakuwako aliyemwonea ndugu yake uchungu. Wakajikatia kuumeni, lakini njaa haikuondoka; wakala nako kushotoni, lakini hawakushiba; kisha wakala kila mtu nyama ya mkono wake: Manase akamla Efuraimu, naye Efuraimu akamla Manase, kisha wote wawili pamoja wakamgeukia Yuda. Lakini kwa hayo yote makali yake hayajatulia bado, nao mkono wake ungaliko umekunjuka. Yatawapata wenye hukumu wanaopotoa hukumu, nao waandishi wanaoandika makorofi! Hutaka kuwazuia wanyonge, wasije shaurini, huyapokonya yawapasayo wakiwa wao walio ukoo wangu; tena hutaka, wajane wawe mateka yao, nao wafiwao na wazazi huwanyang'anya mali zao. Siku ya kukaguliwa itakapofika, mtafanya nini, upepo wa kimbunga utokao mbali utakapovuma? Mtamkimbilia nani, awasaidie? Nayo matukufu yenu mtayapeleka wapi, myafiche? Nanyi hamtaona mzungu kuliko huu: kupiga magoti kwenye mateka au kutupwa kwenye mizoga. Lakini kwa hayo yote makali yake hayajatulia bado, nao mkono wake ungaliko umekunjuka. Yatawapata Waasuri nao, ijapo makali yangu yawatumie kuwa fimbo, ijapo machafuko yangu yawe vigongo mikononi mwao. Ninawatuma kujia kabila lililojichafua, ninawaagizia watu, ambao ninawakasirikia, wateke mateka na kuyapokonya mapokonyo, wawakanyage kama matope ya njiani. Lakini wenyewe hawafikiri kama hivyo, wala mioyo yao haina mawazo kama hayo, kwani mioyoni mwao mna neno moja tu: Kuangamiza! Makabila ya watu, wanayotaka kuyang'oa, si machache. Kwani husema: Wakuu wetu wote pamoja sio wafalme? Je? Mji wa Kalno haukuangamia kama ule wa Karkemisi? Mji wa Hamati haukuangamia kama ule wa Arpadi? Nao mji wa Samaria haukuangamia kama ule wa Damasko? Kama mikono yetu ilivyowapata wafalme wa kimizimu na vinyago vyao vilivyokuwa vyenye nguvu kuliko vile vya Yerusalemu na vya Samaria, je? Yale, tuliyowafanyizia Wasamaria na vinyago vyao, yaleyale tusiwafanyizie Wayerusalemu na vinyago vyao? Lakini hapo, Bwana atakapokuwa ameyamaliza matendo yale mlimani kwa Sioni namo Yerusalemu, ndipo, yatakapokuwa aliyoyasema kwamba: Nitauumbua moyo wa mfalme wa Asuri kwa ajili ya uzao wa ukuu wake na kwa ajili ya utukufu wa macho yake wa kujitukuza. Kwani alisema: Nikifanya hayo ni nguvu za mikono yangu, tena ni werevu wangu wa kweli, kwani mimi ni mwenye akili. Mimi nimeondoa mipaka ya makabila ya watu, nikayapokonya malimbiko yao, nikawa ng'ombe mkali, nikawakumba waliokalia viti vya kifalme. Mkono wangu ukaona mali za makabila ya watu, kama wengine wanavyoona vituo vya ndege. Kama watu wanavyookota mayai yaliyoachwa, ndivyo, mimi nilivyookota nchi nzima; nako hakuwako mwenye kupanua bawa, wala mwenye kufumbua kinywa wala mwenye kulia. Shoka litawezaje kujitukuza mbele yake aliyelitumia la kukatia? Au msumeno utawezaje kujikuza mbele yake aliyeutumia wa kukerezea? Ingekuwa kama kusema: Fimbo ndiyo inayompigisha aishikaye, au kama kusema: Kigongo kinamchukua asiye mti. Kwa hiyo Bwana aliye Bwana Mwenye vikosi atatuma kwao wanene jambo litakalowakondesha, nako kwenye utukufu wao kutawaka maunguzo, nayo yataunguza, kama moto unavyounguza. Nao mwanga wa Isiraeli utawawia moto; nao utukufu wao utageuka kuwa kama ndimi za moto; zitayaunguza maboma yao yenye mibigili na mikunju, yateketee kwa siku moja tu. Hivyo atauangamiza utukufu wa misitu na wa mizabibu yao, kuanzia shinani mpaka kwenye nyama za ndani, itazimia, kama mwenye kufa anavyozimia. Miti ya misitu yao itakayosalia itahesabika, mtoto ataweza kuiandika. Siku ile waliosaa wa Isiraeli nao waliopona wa mlango wa Yakobo hawatajishikiza tena kwake yeye aliyewapiga, ila watajishikiza kweli kwa Bwana aliye Mtakatifu wa Isiraeli. Watakaosalia kuwa sao la Yakobo ndio watakaomgeukia Mungu mwenye nguvu. Ijapo wawe wengi kama mchanga wa ufukoni, wao walio ukoo wako wa Isiraeli, watakaomgeukia watakuwa sao tu; wengine angamizo lao litatimizwa, liyatokeze maamuzi yake kuwa ya kweli kabisa. Kwani atakayelitimiza shauri la angamizo ni Bwana Mungu Mwenye vikosi, atavifanyiza katika nchi zote. Kwa hiyo Bwana Mungu Mwenye vikosi anasema hivyo: Mlio ukoo wangu ukaao Sioni, msimwogope Mwasuri, ijapo awapige vigongo, awainulie fimbo yake na kuishika njia ya Wamisri. Kwani bado kitambo kidogo ndipo, machafuko yatakapokoma, makali yangu yawageukie wao, yawamalize. Bwana Mwenye vikosi anawashikia mjeledi, awapige, kama alivyowapiga Wamidiani kwenye Mwamba wa Kunguru, atawainulia nayo fimbo yake, kama alivyoiinulia Wamisri baharini. Siku ile mizigo yao itaondoka mabegani kwenu, nayo miti yao ya kuwafunga itaondoka shingoni kwenu, itavunjika tu kwa unene, mtakaoupata tena. Watakapokuja watapita Ayati, wavuke Migroni, wataiacha mizigo yao Mikimasi. Kisha watapita katika lango la magenge, Geba wapige makambi ya kulala usiku, Warama watatetemeka, wa Gibea wa Sauli watakimbia. Pigeni yowe, ninyi wa binti Galimu! Ninyi wa Laisi, sikilizeni! Nanyi wa Anatoti na mwone ukiwa! Wa Madimena watatawanyika, wakaao Gebimu watakimbia. Siku ya kusimama kwao kule Nobu watainyosha mikono yao, wauteke mlima wa binti Sioni nacho kilima cha Yerusalemu. Bwana aliye Bwana Mwenye vikosi atakapotokea, ayakate matawi yao kwa nguvu zake zitishazo, ndipo, itakapovunjika nayo miti iliyokwenda juu sana, hiyo mirefu yenyewe itaanguka. Navyo vichaka vya mwituni vitakatwa kwa vyuma vikali, mwitu wa Libanoni utaishia kwa nguvu za mwenye utukufu. Mche utamea shinani mwa Isai, kijiti kilichotoka mizizini mwake kitazaa matunda; nayo Roho ya Bwana itamkalia: ni roho yenye werevu wa kweli na utambuzi, ni roho yenye mizungu na uwezo, ni roho ya kumjua Bwana nayo ya kumcha. Naye atapendezwa na kumcha Bwana, hataamua kwa hayo, macho yake yatakayoyaona, wala hatakata mashauri kwa hayo, masikio yake yatakayoyasikia. Atawaamulia wanyonge kwa wongofu, nao wakiwa atawakatia mashauri yanyokayo, nazo nchi atazipiga kwa fimbo ya kinywa chake, nao wasiomcha Mungu atawaua kwa pumzi itokayo midomoni mwake. Wongofu utakuwa mkanda wake wa kujifunga, nao welekevu utakuwa mshipi wa kiunoni pake. Hapo mbwa wa mwitu watafikia kwenye wana wa kondoo, nao chui watalala pamoja na wana wa mbuzi, hata ndama na simba na ng'ombe mnono watalisha pamoja, wakichungwa na mtoto mdogo. Ng'ombe na kukuu watakula pamoja, nao watoto wao watalala pamoja, nao simba watakula majani makavu. Watoto wachanga watacheza penye mashimo ya pili, nao watoto walioacha maziwa ya mama watapeleka vidole vyao machoni kwa nyoka za moto. Hawatafanya mabaya wala mapotovu katika milima yangu yote mitakatifu; kwani nchi zitajaa watu wamjuao Bwana, kama maji yanavyofurika baharini. Siku ile ndipo, wamizimu watakapolitafuta shina la Isai, maana litakuwa bendera, makabila ya watu yakayotwekewa, nayo makao yake yatakuwa yenye utukufu. Siku ile itakuwa mara ya pili, Bwana akiukunjua mkono wake, awakomboe waliosalia kwao walio ukoo wake, awatoe katika nchi zilizo za Asuri na za Misri za chini na za juu na za Nubi na za Elamu na za Sinari na za Hamati nako kwenye visiwa vilivyoko baharini. Hivyo atawatwekea wamizimu bendera, awakusanye Waisiraeli waliotawanyika, awaokote nao wanawake wa Kiyuda waliopotea, atawakusanya na kuwatoa pande zote nne za nchi. Hapo ndipo, wivu wa Waefuraimu utakapokomea, nao waliowasonga Wayuda watang'olewa; Waefuraimu hawatawaonea Wayuda wivu tena, wala Wayuda hawatawasonga Waefuraimu. Wataruka pamoja kama ndege, watue mabegani kwa Wafilisti upande wa baharini, nako upande wa maawioni kwa jua watawateka wakaao huko; nchi za Edomu na za Mowabu watazichukua kwa mikono yao, nao wana wa Amoni watawatii. Hata ulimi wa bahari ya Misri Bwana atautia mwiko, ukauke; nalo lile jito kubwa atalikunjulia mkono wake, alifokee kwa moto wa makali yake, litokee vijito saba, watu waweze kupita pasipo kuvua viatu. Hivyo patakuwa na njia yao walio sao la ukoo wake, itakuwa, kama ilivyokuwa kwao Waisiraeli siku ile, alipowatoa katika nchi ya Misri. *Nakushukuru, Bwana, ya kuwa ulinichafukia, kwani machafuko yako yamegeuka, ukanituliza moyo. Mtazamieni Mungu aniokoaye! Pasipo woga wo wote ninamngojea, kwani Bwana ni nguvu yangu na shangilio langu, yeye Bwana ndiye aniokoaye. Kwa furaha mtachota maji visimani kwenye wokovu. Siku ile mtasema: Mshukuruni Bwana, nalo Jina lake litambikieni! Yajulisheni makabila ya watu matendo yake! Wakumbusheni kwamba: Jina lake ni boma! Mshangilieni Bwana! Kwani hufanya makuu. Hayo sharti yajulikane katika nchi zote! Pigeni shangwe na vigelegele, ninyi mkaao Sioni! Kwani aliye mkuu kwenu katikati ndiye Mtakatifu wa Isiraeli.* Tamko zito la kuwaambia Wababeli, Yesaya, mwana wa Amosi, aliloliona: Twekeni bendera mlimani juu kileleni palipokatwa miti! Walioko karibu wapalizieni sauti na kuwapungia mikono, waje kuingia malangoni mwenye wakuu wa nchi! Wao waliojitakasia mimi nimewaagiza kuja huku, nikawaita nao walio mafundi wangu wa kupiga vita, wapige yowe na kujikuza wakiyatimiza makali yangu. Makelele mengi mno yako milimani kama ni ya watu wengi, sauti za uvumi ziko za wafalme wanaokusanya watu wao. Bwana Mwenye vikosi anavitazama vikosi vyake vya kwenda vitani. Wamekuja na kutoka nchi za mbali mapeoni kwa mbingu, yeye Bwana na vyombo vya machafuko yake vitakavyoziangamiza nchi zote. Pigeni vilio! Kwani siku ya Bwana iko karibu; itakuja kama pigo la umeme, likitoka kwake Mwenyezi. Kwa hiyo mikono yote italegea, nayo mioyo yote ya watu itayeyuka. Vituko na masongano na maumivu yatawashika, wajipinde kama mzazi, watatumbulizana macho kwa kushangaa, nyuso zao zitawaiva kama ni zenye moto. Tazameni: Siku ya Bwana inakuja, inaleta mastuko na makali na machafuko yenye moto, yaziangamize nchi, ziwe jangwa, kwa kuwamaliza wakosaji, wasikae. Kwani nyota za mbinguni kama kilimia na wenziwe hazitaangaza mwanga wao, jua nalo litakapokucha litakuwa jeusi lenye giza, nao mwezi hautaumulikisha mwanga wake. Nitayaumbua mabaya kwao wakaao nchini, nayo mapotovu yao kwao wasionicha, niyanyamazishe majivuno yao wajitutumuao, niwanyenyekeze wakorofi wajiwaziao kuwa wakuu. Nitafanya, watu wawe wachache kuliko dhahabu, kweli wenye kufa watakuwa haba kuliko dhahabu ya Ofiri. Kwa sababu hii nitazitikisa mbingu, nayo nchi itatenguliwa mahali pake kwa kutetemeka, makali ya Bwana Mwenye vikosi yatakapotokea, siku ya kuyaleta machafuko yake yenye moto itakapotimia. Watakuwa kama paa akimbiaye kwa kustushwa au kama kondoo wakosao mchungaji; ndivyo, watakavyowageukia kila mtu wenziwe wa kwao, ndivyo, watakavyokimbilia kila mtu shamba lake. Kwani kila atakayeonekana atachomwa, kila atakayekamatwa atauawa kwa upanga. Nao watoto wao wachanga watapondwa machoni pao, nyumba zao zitatekwa, wanawake wao watatiwa soni. Jueni, nitawaletea Wamedi wasiotaka fedha, wasiopendezwa na dhahabu. Lakini pindi zao hupiga vijana, wafe; hata wenye mimba hawawaonei huruma, wala macho yao hayatazami watoto, waache kuwaua. Kweli Babeli umekuwa urembo wa wafalme nao utukufu, Wakasidi waliojivunia, lakini Mungu atauangamiza, kama alivyoiangamiza miji ya Sodomu na ya Gomora. Hautakaa kale na kale, wala havitatua humo vizazi na vizazi, Waarabu tu hawatapiga mle mahema yao, wala wachungaji hawatawapumzisha kondoo wao hapohapo. Ila nyama wa porini watalala hapo, nyumba zao zitajaa mabundi, nao mbuni watalala huko, hata mashetani watachezacheza hapo. Mbwa wa mwitu watalia majumbani mwao, nao mbweha katika nyumba zao zilizokuwa na furaha tu. Kweli mwisho wa mji huo uko karibu kutimia, siku zake hazitakawilia. Kwani Bwana atawahurumia wa Yakobo, atawachagua Waisiraeli tena, awarudishe katika nchi yao, watue kuko huko, hata wageni wataandamana nao, wajitie katika mlango wa Yakobo. Watu wengine watawachukua, wawapeleke kwao, kisha mlango wa Isiraeli utawatumia katika nchi ya Bwana kuwa watumishi wao wa kiume na wa kike. Hivyo watawateka waliowateka, wawatawale waliowasonga. Hapo Bwana atakapokupatia pa kutulia na kuyapumzikia masumbufu na mahangaiko na matumishi yako magumu, waliyokutumikisha, utamwimbia mfalme wa Babeli wimbo huu wa kumfyoza kwamba: Kumbe mwenye kusonga ametulia! Kumbe napo tulipoumizwa pametulia! Bwana amezivunja fimbo zao wasiomcha, fimbo zao waliotutawala! Ni zile fimbo zao walioyapiga makabila ya watu kwa ukali pasipo kukoma. Ni fimbo zao walioponda mataifa mazima wakiyakanyaga kwa ukali tu pasipo huruma. Nchi yote nzima imetulia kimya, wote pia wanapiga shangwe. Hata mivinje imefurahi pamoja na miangati ya Libanoni kwamba: Tangu hapo ulipotulizwa hakuna aliyepanda kutukata. Kule chini kuzimuni kumevurugika kwa ajili yako: kwa kungoja, uje, kukawaamsha wazimu wote, waliokuwa wenye nguvu katika nchi, kukawainua wafalme wote, wao wa kimizimu, waondoke katika viti vyao vilivyo vya kifalme. Wote pamoja wanakuzomea kwamba: Kumbe nawe umegeuzwa kuwa mnyonge kama sisi! Ukafananishwa kuwa sawasawa kama sisi! Kumbe nao utukufu wako umekumbwa kushuka kuzimuni pamoja na milio ya mapango yako! Chini umetandikiwa funyo kuwa kilalio chako, nalo blanketi lako la kujifunika ni vidudu. Kumbe umeanguka toka mbinguni, ulimokuwa nyota yenye mwanga uliokuwa kama mwanga wa macheche ya jua! Kumbe umepondwa, ukaanguka chini uliyeyalaza mataifa chini yako! Nawe ulijiwazia moyoni mwako kwamba: Na nipande mbinguni kwenye nyota za Mungu, nikisimike kiti changu cha kifalme huko juu, nikae mlimani kwa miungu mapeoni kwa kaskazini! Na nipande kupita mawingu yaliyoko mbinguni juu, nijifananishe kuwa sawasawa naye Mwenyezi! Kumbe umeshushwa kuzimuni mapeoni kwenye mashimo! Wakuonao watakutumbulia macho, wakutambue kwamba: Je? Huyu siye aliyeitetemesha nchi, aliyewatikisa nao wafalme? Je? Siye aliyezigeuza nchi kuwa mapori tu? Je? Siye aliyebomoa miji mizima? Je? Siye aliyewakataza wafungwa wake, wasirudi kwao? Wafalme wote wa kimizimu hulala kwenye utukufu, kila mtu chumbani mwake; lakini wewe umetupwa mbali, usifike kaburini mwako, ukawa kama tawi litapishalo watu, ukafunikwa na mizoga yao waliochomwa kwa panga, waliotupwa mashimoni kwenye majiwe, ukawa kama kibudu kinachokanyagwa. Wewe hutafika kaburini pamoja nao wale, kwani nchi yako umeiangamiza, nao walio ukoo wako umewaua. Uzao wao wasiomcha hautatajwa kale na kale. Watu husema: Na tuwatengenezee wana wao pa kuwachinjia kwa ajili ya manza, baba zao walizozikora, wasije kuinuka tena na kutwaa nchi na kupajaza hapa juu nchini miji yao! Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Nitawainukia, niling'oe jina la Babeli nalo sao lake, wanawe na wajukuu; ndivyo, asemavyo Bwana. Nitaiweka nchi yao kuwa kao lao nungu, iwe yenye mabwawa ya matopetope tu; nitapazoa kabisa na kutumia kizoleo kiangamizacho! Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Bwana Mwenye vikosi ameapa kwamba: Kama nilivyoyawaza moyoni, yatakuwa vivyo hivyo; kama nilivyokata shauri, yatatimia vivyo hivyo. Nitawaponda Waasuri katika nchi yangu, nitawamaliza na kuwakanyagakanyaga mlimani kwangu. Mizigo yao iondoke kwao wanaokaa kule, hata miti ya kuchukulia mizigo iondoke kwao mabegani. Hili ndilo shauri, alilozipigia nchi zote; kwa hiyo mkono wake uko umewakunjukia wamizimu wote. Kwani Bwana Mwenye vikosi akikata shauri, yuko nani atakayelitangua? Yuko nani atakayeukunja mkono wake uliokunjuka? Mwaka ule, mfalme Ahazi alipokufa, tamko hili zito likatokea: Ninyi wa nchi nzima ya Ufilisti, msifurahie kwamba: Fimbo iliyotupiga imevunjika! Kwani kooni mwa nyoka atatoka pili, naye atazaa nondo mwenye mabawa. Hapo ndipo, wanyonge waliosongeka sana watakapolisha, nao wakiwa watalala hapohapo na kutulia vizuri; lakini mizizi yako nitaifisha kwa njaa, nao watakaosalia atawaua yule nondo. Piga kilio, wewe lango! Omboleza, wewe mji! Zimia, nchi nzima ya Ufilisti! Kwani uko moshi utakaotoka kaskazini, kwao asiwe atakayeachwa peke yake kambini. Nao majumbe wa taifa la kimizimu watapata jibu gani? Ni hili: Bwana ameushikiza Sioni! Wanyonge wao walio ukoo wake watapakimbilia! Kumbe Ari wa Moabu umebomolewa usiku, ukaangamia! Kumbe Kiri wa Moabu nao umebomolewa usiku! Wabeti na Wadiboni wanapanda vilimani kupiga vilio; kule Nebo na Medeba Wamoabu wanaomboleza, vichwa vyao vyote viko na vipara, nazo ndevu zote zimekatwa. Wakitoka nje huwa wamejivika magunia, wao wote, kama wamo vipaani au kama wamo mawanjani, wanapiga vilio na kutoa machozi. Wahesiboni na Waelale wanapiga makelele, sauti zao zinasikilika mpaka Yasa. Kwa hiyo nao wapiga vita wa Moabu wanapiga yowe, maana mioyo yao imekwisha kuwa mibaya. Moyo wangu unawalilia Wamoabu, kwa kukimbizwa wamefika Soari na Eglati wa tatu, hata njia za Luhiti watu wanazipanda na kulia, vilevile njiani kwenda Horonemu wanapiga makelele ya kuyalilia maangamizo. Kwani maji ya Nimurimu yamekupwa, pakawa nyika, majani ya hapo yamenyauka, malisho yamekauka, hakuna kitakachoota hapo tena. Kwa sababu hii wanayapeleka masao ya mali zao, hata malimbiko yao, wayavushe mtoni huko nyikani. Vilio vimezunguka kwenye mipaka yote ya Moabu, maombolezo yao yanasikilika mpaka Eglemu, hata Beri-Elimu yamefika maombolezo yao. Kwani maji ya Rimoni yamejaa damu; nao Wamoabu waliokimbilia Dimoni nitawaletea kibaya kingine: ni simba atakayewamaliza pamoja nao waliosalia katika nchi yao. Watumeni wana kondoo wapasao mtawala nchi, watoke magengeni, wapite nyikani, wafike mlimani kwa Binti Sioni! Kama ndege wanavyohangaika na kurukaruka wakistushwa matunduni mwao, ndivyo, wana wa Moabu watakavyokuwa na kuvikimbilia vivuko vya Arnoni. Tupatieni mzungu! Tupatanisheni! Vikuzeni vivuli vyenu vya mchana, viwe virefu kama vya jioni, viwe maficho yao wafukuzwao! Msiwachongee waliokimbia! Acha, wafukuzwao Moabu wafikie kwako! Wawie ficho machoni pao wanaowakimbiza, sharti siku zao wawasongao ziishe, maangamizo yamalizike, nao waliowaponda watoweke katika nchi yao! Hapo kiti cha kifalme kitasimikwa kwa upole, naye atakayekikalia kwa welekevu hemani mwa Dawidi atakuwa mwamuzi atafutaye yanyokayo kwa kujua wongofu. Tuliyasikia majivuno ya Wamoabu kuwa makuu sana, lakini hayo matukuzo na majivuno na machafuko yao ni maneno makuu tu. Kwa hiyo Wamoabu wote pamoja na waipigie kilio nchi yao ya Moabu, na wayalilie maandazi ya zabibu ya Kiri-Hereseti kwa kupondeka rohoni. Kwani mashamba ya Hesiboni yamenyauka, hata mizabibu ya Sibuma iliyoleta zabibu zenye mvinyo kali za kulevya nao wakuu wa wamizimu; matawi yao yaliendelea sana, yakafika Yazeri, mengine yakapotea nyikani, miche yao ikaenea po pote mpaka kwenye bahari. Kwa hiyo nami ninaililia mizabibu ya Sibuma pamoja na watu wa Yazeri, machozi yangu yazinyeshee nchi za Hesiboni na za Elale, kwani mazomeo yamewaangukia siku hizi za kiangazi zilizo siku zenu za mavuno yenu. Shangwe za furaha zikatoweka mashambani, nako mizabibuni hawapigi vigelegele wala mashangilio, wala hakuna anayekamulia mvinyo makamulioni, nyimbo za wakamuliaji nimezinyamazisha. Kwa hiyo nasikia ndani yangu mlio kama wa zeze wa kuwalilia Wamoabu, namo kufuani umo mlio wa kuwalilia watu wa Kiri-Heresi. Napo hapo, Wamoabu watakapotokea vilimani juu na kujisumbulia hapohapo, napo, watakapoingia patakatifu pao kuomba, hakuna watakachojipatia. Hilo ndilo tamko zito, Bwana alilolisema kale la kuwaambia Wamoabu; lakini sasa Bwana anasema hivi: Itakapotimia miaka mitatu iliyo kama miaka ya kibarua, ndipo, utukufu wa Moabu utakapokuwa umebezeka, nao ulikuwa haukupimika kwa wingi wa watu, nalo sao lao litakuwa limepunguka, liwe dogo sana pasipo nguvu zo zote. Na mwone, mji wa Damasko ukiondolewa, usiwe mji, utakuwa chungu la mawe yatawanyikayo. Miji ya Aroeri itakuwa imeachwa nayo, itakuwa malisho, makundi yatapumzikia hapo pasipo kuona atakayeyastusha. Hivyo ngome ya Efuraimu itapotea, ufalme utakapoondoka Damasko, nalo sao la Ushami litakuwa kama utukufu wa Waisiraeli; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Siku ile ndipo, utukufu wa Yakobo utakapopunguka sana, nao mwili wake mnene utakuwa gofu la mtu tu. Itakuwa kama mvunaji akishika manyasi, mkono wake ukate masuke, au itakuwa kama mtu akitaka kuokota masuke katika bonde la Refaimu. Watakaosalia watakuwa wa kuokoteza, itakuwa kama penye mavuno ya matunda ya mchekele: mawili matatu yatasalia kileleni juu kabisa, manne matano yatasalia katika matawi ya mti, ulioyazaa; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu wa Isiraeli. Siku ile watu watamtazamia tena aliyewaumba, macho yao yatamwelekea Mtakatifu wa Isiraeli; hawatapatazamia tena mahali pao pa kutambikia, mikono yao ilipopatengeneza, wala hawatataka kuiona tena mifano ya mwezi wala ya jua, waliyoifanya kwa vidole vyao. Siku ile miji yenu yenye maboma itageuka kuwa kama mahame ya mwituni au ya milimani, waliyoyaacha walipowakimbia Waisiraeli, maana itakuwa peke yao tu pasipo watu. Kwani umemsahau Mungu aliye wokovu wako, hukuukumbuka mwamba ulio nguvu yako. Kwa hiyo panda tu mashamba ya kupendeza na kumwaga mle mbegu za miti migeni! Siku ya kupandia uzichipuze, kesho zipate kuchanua! Lakini mavuno yatakuwa yamekimbia siku ile, utakapougua kwa kupatwa na maumivu yasiyopona. Je? Uvumi gani huu wa makabila mengi ya watu? Wanavuma, kama maji yanavyovuma yakiwa mengi. Ni ngurumo gani ya makabila ya watu? Wananguruma kama ni ngurumo ya maji yenye nguvu. Lakini ijapo makabila ya watu yangurume, kama maji mengi yanavyonguruma, yeye atakapowakaripia, watakimbia mbali sana, watafukuzwa, waruke kama makapi, yakipeperushwa na upepo vilimani juu, au kama mavumbi, yakichukuliwa na kimbunga. Ilipokuwa jioni, mastuko yakawa yangaliko bado, lakini kulipotaka kupambazuka, yalikuwa yametoweka. Hilo ndilo fungu lao waliotaka kututeka, hilo ndilo gawio, kura lililowapatia wao waliotaka kuzipokonya mali zetu. Ninyi mliotoka katika nchi yenye vivuli viwili iliyoko ng'ambo ya majito ya Nubi! Ninyi wajumbe mliokuja mkilifuata lile jito kubwa katika mitumbwi yenu ya mafunjo ya kwendea juu ya maji, ninyi wajumbe wepesi, nendeni kwenu kwenye watu warefu sana wajipakao mafuta. Ndio watu wanaoogopwa kwao hata kungineko, kwa kuwa ni wenye nguvu za kuponda watu, nayo nchi yao inakatwakatwa na mito. Nyote mkaao ulimwenguni, nyote mliotua nchini, bendera itakapotwekwa milimani, itazameni! Mabaragumu yatakapopigwa, yasikilizeni! Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu wangu anavyosema: Nitatulia, nichungulie kwenye kao langu kama mwangaza mweupe wa jua kali la mchana, au kama wingu lenye umande siku za mavuno. Kwani mavuno yanapokuwa hayajafika bado, maua yakiisha kupakatika, kole likiivisha zabibu zake, ndipo, anapoyakata kwa kisu matawi yenye majani tu, ndipo, anapoiondoa miche, itoke kabisa. Wote pamoja wataachiliwa madege wakaao milimani nao nyama wa porini, madege makubwa wakae hapo siku za kiangazi, nao nyama wote wa porini wawe hapo siku za kipupwe. Siku zile Bwana Mwenye vikosi ataletewa matunzo nao walio watu warefu sana wajipakao mafuta. Ndio wale watu wanaoogopwa kwao na kungineko, kwa kuwa ni watu wenye nguvu za kuponda watu, nayo nchi yao inakatwakatwa na mito. Hao watatua matunzo yao mahali penye Jina la Bwana Mwenye vikosi, ndipo mlimani kwa Sioni. Tazameni: Bwana amepanda wingu jepesi, aje Misri! Vinyago vya Misri vinatikisika usoni pake, mioyo yao Wamisri imeyeyuka vifuani mwao. Nitawachochea Wamisri, wapigane na Wamisri wenzao, wagombane mtu na ndugu yake, hata mtu na mwenziwe, hata mji upigane na mji mwingine, vilevile ufalme ugombane na ufalme mwingine. Hapo ndipo, roho zao Wamisri zitakapozimia vifuani mwao, nikiitengua mizungu yao; nao watatafuta msaada kwa vinyago na kwa waganga, kwa wachawi na kwa waaguaji. Nitawafungia Wamisri mikononi mwa bwana mgumu, mfalme, mwenye ukorofi, awatawale! Ndivyo, asemavyo Bwana aliye Bwana Mwenye vikosi. Kisha maji yatakupwa baharini, nao mto mkubwa utakauka, pawe pakavu tu. Mifereji mikubwa ya maji itanuka vibaya, nayo mito ya Misri ya chini itakuwa minyonge, kisha itakauka nayo, hata matete na manyasi yatanyauka. Viwanda vilivyoko kando ya mto kwenye kingo za mto, nayo mashamba yote ya mtoni yatanyauka, yatakauka kabisa yatoweke. Wavuvi watalia, pamoja nao wote waliokamata samaki mtoni kwa ndoana watasikitika, nao waliotanda nyavu majini watafifia. Hata wafanyao kazi za pamba wataangamia pamoja nao wafumao nguo nyeupe. Hivyo misingi yao itakuwa imepondeka, wote wafanyao kazi za kibarua wataumia rohoni. Wakuu wa Soani watakuwa wamepumbaa kabisa; nao wajuzi wa Farao wasiokosa mizungu, hapo mizungu yao itakuwa ujinga tu. Mtawezaje kumwambia Farao: Mimi ni mwana wao watambuzi? au: Mimi ni mwana wao wafalme wa kale? Sasa watambuzi wako wako wapi? Kama wanalitambua, na wakufumbulie shauri, Bwana Mwenye vikosi aliloikatia nchi ya Misri! Wakuu wa Soani ni wajinga kweli, nao wakuu wa Nofu wamedanganyika, waliokuwa vichwa vya milango wameiangamiza Misri. Bwana amemwaga mioyoni mwao roho za kizunguzungu, wawapoteze Wamisri katika matendo yao yote, wapepesuke kama mlevi kwenye matapiko yake. Hakuna tendo tena, Wamisri, watakalolitenda, kama ni kichwa au mkia, kama ni makuti au majani. Siku zile Wamisri watakuwa kama wanawake, watetemeke kwa kuyastukia matisho ya mkono wa Bwana Mwenye vikosi, atakaowakunjulia. Hapo nchi ya Yuda itawawia Wamisri kitisho, kila mtu aingiwe na kituko atakaposikia, ikitajwa, kwa ajili ya shauri la Bwana Mwenye vikosi, alilowakatia. Siku ile miji mitano itakuwako katika nchi ya Misri itakayosema msemo wa Kanaani, itakayoapa na kulitaja Jina la Bwana Mwenye vikosi, mmoja wao utaitwa Mji wa Mabomoko. Siku zile patakuwako pa kumtambikia Bwana katika nchi ya Misri katikati na nguzo ya Bwana iliyojengwa kwa mawe mpakani kwake. Hivyo Bwana Mwenye vikosi atakuwa na kielekezo cha kumshuhudia katika nchi ya Misri; napo, watakapomlilia Bwana kwa ajili yao wawasongao, atatuma mwokozi, awagombee, awaponye. Ndivyo, Bwana atakavyojulikana kwa Wamisri, kweli Wamisri watamjua Bwana siku zile, watamtumikia na kumtolea ng'ombe za tambiko na vipaji vingine vya tambiko, nayo waliyomwagia Bwana kumpa, watayalipa. Itakuwa hivyo: Bwana akiwapiga Wamisri na kuwaponya, nao wakimrudia Bwana, atawaitikia, wakimwomba, awaponye kabisa. Siku zile itakuwako barabara toka Misri kwenda Asuri, nao Waasuri watakuja Misri, nao Wamisri watakuja Asuri kuamkiana, hivyo Wamisri na Waasuri watatumikiana. Siku zile Isiraeli atakuwa wa tatu wa kupatana na Misri na Asuri, hawa watakuwa mbaraka katika nchi katikati. Naye Bwana Mwenye vikosi atawabariki na kusema: Wabarkiwe Wamisri walio ukoo wangu! Wabarikiwe Waasuri walio kazi ya mikono yangu! Wabarikiwe Waisiraeli walio fungu langu, nililojipatia! Mwaka wake ulipotimia, Sargoni, mfalme wa Asuri, alimtuma Tartani kwenda Asdodi; akapiga vita kule Asdodi, akauteka mji huo. Mwaka uleule Bwana alisema na kumtuma Yesaya, mwana wa Amosi, akamwambia: Nenda, uvue gunia, ulilolifunga kiunoni juu, navyo viatu uvivue miguuni! Akafanya hivyo, akatembea akiwa mwenye uchi wa kifuani na miguuni. Bwana akasema: Kama mtumwa wangu Yesaya alivyotembea akiwa mwenye uchi wa kifuani na miguuni miaka mitatu kuwa kielekezo cha kuwaonya Wamisri nao Wanubi, ndivyo, mfalme wa Asuri atakavyopeleka mateka ya Misri nao Wanubi watakaokamatwa, vijana na wazee, waende wenye uchi vifuani na miguuni, hata matakoni, Wamisri watiwe soni. Hapo watu watastuka na kuingiwa na soni kwa ajili ya Wanubi, waliowatazamia, na kwa ajili ya Wamisri, ambao walijivunia. Nao wakaao kule pwani watasema siku ile: Tazameni, wale, tuliowatazamia, walivyo! Nasi twalitaka kukimbilia kwao, watusaidie, tujiponye machoni pake mfalme wa Asuri. Hivyo tungeponaje sisi? Kama upepo wenye nguvu unavyovuma upande wa kusini, ndivyo, mambo yanavyotoka nyikani katika nchi inayoogopwa. Nimefumbuliwa na kuonyeshwa yenye ugumu: mdanganyifu hudanganya, naye mwangamizaji huangamiza. Pandeni, Waelamu! Shambulieni, Wamedi! Hivyo nitawanyamazisha wote waliowapigia kite. Kwa hiyo viuno vyangu vimeenea kukauka, uchungu ukanishika kama uchungu wa mwanamke azaaye, kizunguzungu kikanipata, nisisikie, nikastushwa, nisione. Roho yangu ikazimia, mastuko yakanigundua; saa za jioni, nilizozipenda, zikawa za kunitetemesha. Wao hutandika meza, huweka wangoja zamu, hula, hunywa. Mara wanaambiwa: Inukeni, wakuu! Zipakeni ngao mafuta! Kwani ndivyo, Bwana alivyoniambia: Nenda, uweke mlinzi, akuambie, atakayoyaona! Atakapoona kikosi cha watu waliopanda farasi, wakienda wawiliwawili, hata kikosi cha punda na kikosi cha ngamia, na aangalie sana kwa uangalifu mwingi. Akaita na kupaza sauti kama simba kwamba: Bwana, hapa kilindoni mimi ninasimama mchana kutwa, nao usiku kucha nimewekwa mimi kungoja hapa kidunguni. Sasa tazameni! Panakuja kikosi cha watu waliopanda farasi wakienda wawiliwawili! Kisha akasema: Umeanguka! Umeanguka mji wa Babeli! Navyo vinyago vyake vyote vya miungu yao amevivunja na kuvitupa chini. Ninyi wenzangu mliopigwa, kama mpunga unavyopigwa penye kuupuria, niliyoyasikia kwa Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, nimewatangazia ninyi. Tamko zito la kuwaambia Waduma: Toka Seiri wananiita kwamba: Mlinzi, saa ngapi sasa za usiku? Mlinzi, saa ngapi sasa za usiku? Mlinzi akajibu: Ijapo mapema yaje, usiku utakuwa ungalipo. Kama mnataka kuuliza mengine, haya! Ulizeni! Tamko zito la kuwaambia Waarabu: Sharti mlale kwenye mapori nyikani, ninyi watembezi wa Dedani! Waliokufa kiu wapelekeeni maji, ninyi mkaao katika nchi ya Tema! Waliokimbia wagawieni vilaji vya kuwatunza! Kwani wamezikimbia panga, zile panga walizochomolewa wao, wamezikimbia nazo pindi, walizovutiwa, hata uzito wote wa vita. Kwani ndivyo, Bwana alivyoniambia: Ungaliko bado mwaka, kama miaka ya kibarua ilivyo, ndipo, utukufu wote wa Kedari utakapokuwa umekwisha. Watakaosalia kwa wana wa Kedari walio wenye nguvu katika hesabu yao ya wavuta pindi watakuwa wachache, kwani Bwana Mungu wa Isiraeli amevisema. Mmeona nini mkipanda wote vipaani? Wewe mji uliojaa makelele ya machafuko, mliomo na wapiga vigelegele, watu wako waliouawa hawakuuawa kwa panga, wala hawakufa vitani. Wakuu wako wamekimbia wote pamoja, wakatekwa pasipo upindi, nao watu wako waliopatikana wametekwa wote, nao waliokimbia mbali. Kwa hiyo nimesema: Msinitumbulie macho, nilie kwa uchungu! Wala msinibembeleze na kunituliza moyo kwa ajili ya kuangamia kwao walio wazaliwa wa ukoo wangu! Kwani siku ya mastuko na ya maangamizo na ya machafuko imetoka kwake Bwana Mungu Mwenye vikosi, ikaja Bondeni kwenye Maono, ni siku iliyobomoa maboma, vilio vyake vikasikilika mlimani. Waelamu wameshika mapodo, wakapanda magari na farasi, Wakiri nao wakazifunua ngao. Ndipo, mabonde yako mazuri yalipojaa magari, nao wapanda farasi wakajisimamisha upande wa lango la maji. Hivyo akayafunua, ambayo Wayuda walijifunika nayo, siku ile wakayatazamia mata yaliyowekwa katika nyumba ya mwituni. Mkapaona, mji wa Dawidi ulipobomokabomoka, ya kuwa ni pengi, mkayakusanya maji ya ziwa la chini. Mkazihesabu nazo nyumba za Yerusalemu, mkabomoa nyingine, mpate ya kuujengajenga ukuta wa boma. Katikati ya kuta mbili za boma mkatengeneza mahali, pawe pa kukusanyia maji ya ziwa la kale. Lakini yeye aliyeyafanya mambo hayo hamkumtazama, hamkumwona aliyeyalinganya, yalipokuwa yangaliko mbali. Bwana aliye Bwana Mwenye vikosi aliwaita siku ile, mlie na kuomboleza, mnyoe vichwa na kuvaa magunia. Kumbe mkacheza na kufurahi, mkaua ng'ombe, mkachinja nao kondoo, mkala nyama, mkanywa mvinyo, mkasema: Na tule, na tunywe! Kwani kesho tutakufa! Kwa hiyo Bwana Mwenye vikosi ameyafumbua masikioni mwangu: Mpaka mtakapokufa, hamtaondolewa kabisa manza hizi, mlizozikora. Ndivyo, anavyosema Bwana Mungu Mwenye vikosi. Ndivyo, anavyosema Bwana Mungu Mwenye vikosi: Nenda, uje kwake huyo mtunza mali, huyo Sebuna aliye mkuu wa nyumba ya mfalme. Unafanya nini hapa? Kuna nani wa kwenu huku? Kumbe unajichimbia kaburi hapa! Kweli unajichimbia hapa juu kaburi lako, unajichongea magengeni kao lako! Tazama, Bwana atakutupa na kukubwaga kwa nguvu! Wewe mtu wa kiume atakukunja kabisa. Atakuzinga, uviringane kama mpira, akutupe katika nchi iliyopanuka pande mbili; ndiko, utakakokufa, ndiko, magari yako mazuri yatakakokufuata wewe uliyeitweza Nyumba ya Bwana wako. Nitakutangua katika utunzaji wako, nitakuondoa katika usimamizi wako. Siku ile ndipo, nitakapomwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia. Nitamvika kanzu yako, nitamfunga nao mshipi wako, utunzaji wako nitampa, uwe mkononi mwake, atakuwa baba yao wakaao Yerusalemu, hata baba yao walio wa mlango wa Yuda. Nitampa ufunguo wa nyumba ya Dawidi, uwe begani pake; atakapofungua, hatakuwako awezaye kupafunga, atakapofunga, hatakuwako awezaye kupafungua. Nitampigilia kama msumari mahali pagumu, atauwia lango wa baba yake kiti chenye utukufu. Kwake utatundikwa utukufu wote wa mlango wa baba yake; miche na machipukizi na vyombo vyote vidogo, kuanzia vikombekombe kufikisha mitungitungi yote. Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Msumari uliokuwa umepigiliwa mahali pagumu siku ile uvunjike, utajipinda, uanguke chini, nao mzigo ulioangikwa kwake utaanguka, kwani Bwana amevisema. Pigeni vilio, ninyi merikebu za Tarsisi! Kwani mji wenu umetoweshwa, hamna nyumba wala kituo; ndivyo, walivyoambiwa katika nchi ya Wakiti. Nyamazeni, ninyi mkaao pwani! Wachuuzi wa Sidoni waliopita baharini waliwaletea yote. Kwenye maji mengi uliletewa yaliyopandwa Sihori nayo yaliyovunwa mtoni kwa Nili, ukawa mahali, mataifa yalipochuuzia. Ona soni, Sidoni! Kwani baharini kwenye ngome ya baharini wako waliolia kwamba: Sikushikwa na uchungu, sikuzaa, wala sikulea vijana, wala sikukuza wanawali. Wamisri watakapoyasikia, watashikwa na uchungu kwa kuzisikia hizo habari za Tiro. Vukeni kuja Tarsisi! Pigeni vilio, mkaao pwani! Je? Huo ndio mji wenu uliopiga vigelegele? uliojengwa siku za kale kabisa? ulioiendesha miguu yenu, mwende katika nchi za mbali kutua kulekule? Ni nani aliyeukatia Tiro shauri hili? Ulikuwa umegawia wengine taji za kifalme, wachuuzi wake walikuwa wakuu wa nchi, nao waliokuwa wenye maduka walitukuzwa kuliko wengine katika nchi. Bwana Mwenye vikosi ndiye aliyelikata shauri lake, auchafue urembo wote, waliojivunia, awanyenyekeze wote waliotukuka katika nchi. Furikieni katika nchi yenu kama mto wa Nili, ninyi wana wa Tarsisi! Hakuna ukingo tena. Bwana ameikunjulia bahari mkono wake, akazitetemesha nchi zenye wafalme, akaagiza, miji ya Kanaani yenye maboma ibomolewe. Akasema: Hutashangilia tena, binti Sidoni, kwa kuwa mwanamwali aliyetiwa soni. Ondoka, uvuke kwenda kwao Wakiti! Lakini nako kule hutapata kutulia. Itazameni nchi ya Wakasidi! Ndio watu wasiokuwa kabila; kwa hiyo Waasuri walitaka kuigeuza nchi yao, iwe kao la nyama wa porini. Lakini sasa wanaisimamisha minara yao ya kulindia, wakayabomoa majumba ya nchi hii na kuyageuza kuwa mabomoko. Pigeni vilio, ninyi merikebu za Tarsisi! Kwani mji wenu uliokuwa na nguvu umetoweshwa. Siku zile mji wa Tiro utakuwa umesahauliwa miaka 70, kama siku za mfalme mmoja zilivyo. Miaka 70 itakapokwisha, Tiro utapata yaliyoandikwa katika wimbo wa mwanamke mgoni ya kwamba: Chukua zeze, utembee mjini, wewe mwanamke mgoni uliyesahauliwa! Kalipige zeze vizuri, uliimbie nyimbo nyingi, ukumbukwe tena! Miaka 70 itakapokwisha, Bwana ataukagua mji wa Tiro, uyarudie mapato ya uasherati wake, ukiufuata ugoni katika nchi zote zenye wafalme zilizoko ulimwenguni. Lakini mapato yake ya uchuuzi na ya uasherati yatakuwa mali za Bwana, hazitalimbikwa, wala hazitawekwa za akiba, ila atakayoyapata kwa uchuuzi wake, watagawiwa wakaao machoni pa Bwana, wapate kula na kushiba, tena wapate kuvaa na kujifunika vema. Tazameni, Bwana anaondoa watu katika nchi, iwe peke yake! Anaiumbua umbo lake na kuwatawanya wanaokaa huku. Wote watakuwa sawa: watu na mtambikaji, mtumwa na mabwana wake, kijakazi na bibi yake, anunuaye na auzaye, akopeshaye na akopaye, mwenye kudai na mwenye kudaiwa. Kweli nchi itaondolewa watu kabisa, nazo mali zitapokonywa, kwani Bwana amelisema neno hilo. Nchi imesikitika, maana imenyauka, ulimwengu wote umefifia, maana umenyauka, nao walio wakuu wa watu katika nchi wamefifia. Chini yao wakaao huku nchi imechafuliwa, kwani wameyapita Maonyo, hawakuyafuata maongozi, wakalivunja Agano la kale na kale. Kwa sababu hii apizo limeila nchi; nao wakaao huku wanalipishwa manza, walizozikora; kwa sababu hii waikaao nchi wameunguzwa, watu waliosalia ni wachache tu. Mvinyo mbichi zimesikitika, mizabibu imefifia, wote waliokuwa na furaha mioyoni hupiga kite. Patu zilizofurahisha hunyamaza, makelele yao wapigao vigelegele yamekoma, nayo mazeze yaliyofurahisha hunyamaza. Hawanywi tena mvinyo na kuiimbia, kileo cha sasa ni chenye uchungu kwao wanaokinywa. Mji umebomolewa, uko peke yake tu, kila nyumba imefungwa, hakuna anayekuja. Makelele ya kulilia mvinyo yanasikilika huko nje, furaha yote imeguiwa na giza, maana yote yaliyoifurahisha nchi yamehama. Yaliosalia mjini ni mahame tu, nalo lango lake limevunjwavunjwa kuwa vipandepande tu. Kwani hivyo ndivyo, mambo yatakavyokuwa katika nchi katikati ya watu, kama yalivyo penye mavuno ya matunda ya mchekele au penye kuokoteza, mavuno ya zabibu yakiisha. Hawa wanapaza sauti zao kwa kupiga vigelegele wakiushangilia utukufu wa Bwana kuanzia baharini. Kwa hiyo mtukuzeni Bwana nako maawioni kwa jua, nako kwenye visiwa vilivyoko baharini litukuzeni Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli! Toka mapeoni kwa nchi tulisikia nyimbo kwamba: Mwongofu na apambwe! Nikajibu kwamba: Ni mnyonge! Ni mnyonge! Nimekufa! Wakorofi wanakorofisha, kweli wakorofi wanakorofisha kwa ukorofi. Mastuko na miina na matanzi yanawangoja ninyi mkaao katika nchi! Itakuwa hivi: Atakayeyakimbia makelele ya kustusha ataanguka mwinani, naye atakayepanda na kutoka mwinani atanaswa na tanzi, kwani madirisha ya huko juu yatakuwa yamefunguliwa, nayo misingi ya nchi itatetemeka. Nchi itavunjikavunjika, nchi itaatukaatuka, nchi itayumbayumba. Nchi itapepesukapepesuka kama mlevi, itachukuliwa huko na huko kama machela, italemewa na mapotovu yake, itaanguka, isiweze kuinuka tena. Siku ile itakuwa hivi: Bwana atavijilia vikosi vya juu huko juu, nao wafalme wa nchi atawajilia huku chini. Watakusanywa, kama wafungwa wanavyokusanywa, wapelekwe shimoni, wafungwe kifungoni, tena wafunguliwe, siku nyingi zitakapopita. Hapo ndipo, mwezi utakapojifunika, ndipo, nalo jua litakapoona soni, kwa kuwa Bwana Mwenye vikosi atakuwa yuko mfalme mlimani kwa Sioni namo Yerusalemu, nako mbele ya wazee wake utakuwako utukufu. Bwana, wewe ndiwe Mungu wangu, na nikutukuze, na nilishukuru Jina lako, kwani umefanya mataajabu, mashauri yako ya kale hayakugeuka, yametimia kweli. Kwani mji umeugeuza kuwa chungu la mawe, mji wenye boma ukawa mabomoko, majumba ya wageni hayafikiwi tena, kwani mji hautajengwa kale na kale. Kwa hiyo watu wenye nguvu wanakutukuza, nayo miji ya watu wa kimizimu waliokuwa wenye ukorofi inakuogopa. Kwani umekuwa ngome ya wanyonge na ngome ya wakiwa, waliposongeka, ukawa kimbilio penye kimbunga na kivuli penye jua kali, kwani kufoka kwao wakorofi ni kama kimbunga ukutani, au kama jua kali jangwani. Makelele ya wageni ukayanyamazisha; kama jua kali linavyoshindwa na kivuli cha wingu, ndivyo, shangwe za wakorofi zilivyonyenyekezwa. Bwana Mwenye vikosi atayafanyia makabila yote ya watu karamu ya manono huku mlimani, itakuwa karamu yenye mvinyo kali na vilaji vyenye mafuta ya kiini, nazo mvinyo hizo zitakuwa zimechujwa. Mlimani huku atayatowesha mabuibui ya nyuso, ni mabuibui yaliyoyafunika makabila yote ya watu, hata mafuniko, yaliyotandwa juu ya wamizimu wote. Kufa nako atakumeza, kutoweke kale na kale; kisha Bwana Mungu atayafuta machozi nyusoni pao wote, nayo matwezo yao walio ukoo wake atayaondoa katika nchi zote, kwani Bwana amevisema. Siku ile watasema: Mtazameni huyu! Ndiye Mungu wetu, tuliyemngojea, atuokoe; huyu ndiye Bwana, tuliyemngojea. Na tushangilie! Na tuufurahie wokovu wake! Kwani mkono wake Bwana utatulia mlimani huku, lakini Wamoabu watakanyagwa kwao, kama majani makavu yanavyokanyagwa majini penye mavi. Ijapo wapanue mikono yao mle ndani, kama mwogeleaji anavyoipanua, apate kuogelea. lakini kwa kuwa walijikuza, yeye atawainamisha chini pamoja na mikono yao ihimizayo mizungu ya bure. Hata maboma yenu yenye kuta ndefu atayanyenyekeza, akiyainamisha na kuyaangusha chini uvumbini. Tunao mji ulio wenye nguvu, anatumia wokovu kuwa kuta za boma lake. Yafungueni malango, watu waongofu waingie, washikao welekevu! Mawazo ya moyo yakiwa yamejishikiza, utaendelea kuutengemanisha, utengemane kweli, kwani tumekutegemea. Mtegemeeni Bwana kale na kale! Kwani mnapokuwa naye Bwana Mungu, mnao mwamba wa siku zote za kale na kale. Kwani amewanyenyekeza waliokaa juu mjini mwenye boma, akawainamisha chini kabisa, mpaka akawaangusha uvumbini, wakanyagwe na miguu, ndiyo miguu yao wakiwa na mateke yao wanyonge. Njia ya mwongofu hunyoka, napo pa kupitia, unapomlinganyia mwongofu, huwa pamenyoka. Kweli penye maamuzi yako, Bwana, tulikungojea, roho zetu zikalitunukia Jina lako, likumbukwe. Moyoni mwangu nilikutamani usiku, namo rohoni mwangu ninakutafuta mapema, kwani maamuzi yako yakiitokea nchi, wakaao ulimwenguni hujifunza wongofu. Asiyekucha akihurumiwa hajifunzi wongofu. ila katika nchi yenye mambo yanyokayo, huendelea kuyapotoa, lakini utukufu wa Bwana hauoni. Bwana, ijapo mkono wako utukuke, hawautazami; na wapatwe na soni wakivitazama, jinsi unavyouhimiza wokovu wa watu. Moto uliowamaliza wabishi wako na uwale nao. Ila sisi, Bwana, utatupa kutengemana, kwani yote, tuliyoyafanya sisi, ni kazi zako, ulizotutendea. Bwana Mungu wetu, kuliko wewe hata mabwana wengine walitutawala, lakini wewe peke yako tunakutangaza, Jina lako likumbukwe. Wafu hawatarudi uzimani, wala wazimu hawatainuka; kweli ulipowajia uliwaangamiza, ukalitowesha kumbukumbu lao lote. Kabila hili umeliongeza, Bwana, umeliongeza kweli, ukalitukuza, ukaipanua mipaka yote ya nchi yake. Bwana, wanaposongeka wanakutokea; ulipowapiga, ndipo, walipokuja kukunong'onezea maneno yao ya kukuomba. Mwenye mimba akifikisha kuzaa hujipinda na kulia kwa uchungu wake, ndivyo, nasi tulivyokuwa mbele yako, Bwana. Tulikuwa na mimba, tukashikwa na uchungu, lakini tulipozaa, ni upepo tu! Hatukuipatia nchi wokovu, wala hawakupatikana wenye kukaa ulimwenguni. Wafu wako watarudi uzimani, miili yao wa kwetu waliokufa itainuka. Amkeni, mshangilie, mlalao uvumbini! Kwani umande utokao kwenye mianga ni umande wako, nchi iwaweke wazimu, wapate kukaa tena. Njoni, mlio ukoo wangu, mwingie vyumbani na kuifunga milango yenu nyuma yenu! Jificheni kitambo kidogo, mpaka hayo mapatilizo makali yatakapopita! Kwani tazameni! Bwana anatoka mahali pake, aje kuwalipisha wakaao katika nchi manza walizozikora. Hapo ndipo, nchi itakapozifunua damu zilizomwagwa kwake, haitawafunika tena waliouawa juu yake. Siku ile Bwana atatokea akishika upanga ulio mgumu na mkubwa na wenye nguvu, amlipishe Lewiatani, ni lile joka limkimbialo; yeye Lewiatani, lile joka la kujizinga kabisa, atamwua pamoja na yule nondo alioko baharini. Siku ile watasema: Mzabibu mzuri! Uimbieni! Mimi Bwana ni mlinzi wake; mara kwa mara ninaunywesha; kusudi mtu asiuharibu, ninaulinda usiku na mchana. Ukali sinao tena; kama ningeona mikunju na mibigili, ningeipelekea vita mara moja, niichome moto yote pamoja; nao watanishika, niwalinde kwa nguvu zangu, wataniomba, watulie kwangu, kweli wataniomba, watulie kwangu. Siku zitakazokuja Yakobo atatia mizizi, Isiraeli atachanua na kuzaa matunda, waueneze ulimwengu wote hayo matunda. Je? Amewapiga, kama alivyowapiga waliowapiga? Au wameuawa, kama walivyouawa waliowaua? Amewagombeza tu na kuwafukuza na kuwatuma, wajiendee, akawakimbiza kwa upepo mgumu siku za kimbunga kilichotoka maawioni kwa jua. Hivyo manza zao, wa Yakobo walizozikora, zimefunikwa kweli, nalo hili ndilo pato la kuwaondolea makosa yao: mawe yote ya mahali pa kutambikia miungu wameyaponda kuwa mavumbi kama ya mawe ya chokaa yaliyobunguliwa, nayo mifano ya mwezi na ya jua haikusimikwa tena. Kwani mji uliokuwa wenye nguvu peke yake tu, ni mahame tu pasipo watu; yalipoachwa, pakawa nyika: ng'ombe wanalisha huko, wanapumzika huko na kuvimaliza vijiti vyake. Matawi yao yakiisha kukauka, huvunjwa; wanawake wanakuja, wanayatumia kuwa kuni, kwani sio watu wanaotambua maana. Kwa hiyo yeye aliyewafanya hawahurumii, muumba wao hawaonei uchungu. Siku ile Bwana atayapura masuke yote, kuanzia kwenye lile jito kubwa kufikisha mpaka mtoni kwa Misri. Nanyi wana wa Isiraeli, mtakusanywa mmoja kwa mmoja. Tena siku ile, baragumu kubwa litakapopigwa, ndipo, wote waliopotelea katika nchi ya Asuri watakapokuja pamoja nao waliotawanyika katika nchi ya Misri, wamtambikie Bwana kwenye mlima mtakatifu wa Yerusalemu. Yatakupata wewe, uliye kilemba chenye majivuno ya walevi wa Efuraimu! Uliye hata sasa urembo wenye utukufu, utakuwa kama ua lililonyauka, kwa maana umejengwa kilimani juu kwenye bonde lioteshalo sana, likaalo watu waangushwao na mvinyo. Tazameni! Mwenye nguvu na ukorofi yuko tayari kwa Bwana, anafanana na mvua ya mawe inayokuja na upepo unaovunjavunja, ni mvua inyeshayo maji mengi yenye nguvu ya kufurikia nchini, nayo yatawabwaga chini na kuwadidimiza kwa kuwavuta kwa nguvu zilizo kama za mkono. Kisha utakanyagwa na miguu, wewe uliye kilemba chenye majivuno ya Efuraimu. Lile ua litakalonyauka lingaliko, nao urembo wenye utukufu wake linao, kwa maana liko kilimani juu kwenye bonde lioteshalo sana, lakini litakuwa kama kuyu inayoiva upesi, siku za mavuno zinapokuwa hazijatimia bado; mtu akiiona anaichuma hapohapo, tena ikiwa ingalimo mkononi mwake, amekwisha kuimeza. Siku ile Bwana Mwenye vikosi atakuwa kilemba chenye urembo na pambo la kipajini lenye utukufu kwao waliosalia wa ukoo wake. Naye atakayekaa kitini penye uamuzi atampa roho yenye unyofu nao wapiga vita watakaowakimbiza adui malangoni atawapa nguvu za kushinda. Kumbe hao nao wanapepesuka kwa mvinyo na kuyumbayumba kwa vileo! Watambikaji na wafumbuaji wanapepesuka kwa vileo: wameshikwa na kizunguzungu kwa kunywa mvinyo, wanayumbayumba kwa vileo, wanapepesuka wakifumbua, wanatukutika wakiamua. Kwani meza zote zimejaa matapiko, hakuna mahali pasipo machafu. Nao husema: Yuko nani, Bwana atakayemfundisha kujua maana? Yuko nani, atakayemtambulisha waliyoyasikia? Ni wao waliozoezwa, waache kunyonya, walioondolewa sasa hivi kwenye maziwa ya wamama? Agizo hufuata agizo, kweli agizo hufuata agizo; kingojeo huita kingojeo, kweli kingojeo huita kingojeo kwamba: Hapa bado kidogo napo hapo bado kidogo! Ni kweli, midomo, watu wasiyoitambua, nazo ndimi zilizo ngeni kwao ndizo, atakazozitumia atakaposema nao walio wa ukoo huu. Maana aliwaambia: Hapo ni penye kupumzikia, waacheni wachovu, wapumzike! Hapa ni penye kutulia! Lakini hawakutaka kusikia. Kwa hiyo lile neno lao litakuwa kwao neno la Bwana: Agizo hufuata agizo, kweli agizo hufuata agizo, kingojeo huita kingojeo, kweli kingojeo huita kingojeo kwamba: Hapa bado kidogo napo hapo bado kidogo! Kusudi waende na kujikwaa na kuanguka kichalichali, wapondeke, wanaswe, watekwe. Kwa hiyo lisikieni neno la Bwana, ninyi waume mfyozao, nanyi mnaowatawala wa Yerusalemu walio wa ukoo huu! Kwani mlisema: Tumekwisha kuagana na kufa, nako kuzimu tumekwisha kupatana nako kwamba: Pigo la kudidimiza litakapokutia, lisitufikie! Kwani uwongo tumeutumia kuwa kimbilio letu, tukajificha kwenye madanganyifu. Lakini hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nitazameni! Mimi ndimi niliyeweka jiwe, liwe msingi wa Sioni, nalo ni jiwe lililojulika, ya kuwa litafaa la pembeni kwa utukufu wake, likawekwa la msingi kuwa kama mwamba, ni hili la kwamba: Alitegemeaye hatakimbia. Nayo yaliyo sawa nikayatumia kuwa kamba ya kupimia, nayo yaongokayo kuwa kipimo chenyewe, mvua ya mawe italiondoa kimbilio lenu la uwongo, nalo ficho lenu maji yatalididimiza. Nayo mliyoyaagana na kufa yatatanguliwa, yasisimamike mliyoyapatana na kuzimu; pigo la kudidimiza litakapotukia, ndipo, watakapopokonywa nalo. Kila mara litakapopita litawashika, kila kunapokucha litapita, hata mchana na usiku; nako kustushwa ndiko peke yake kutakakowatambulisha mliyoyasikia. Kwani: Kitanda kifupi, hutaweza kujinyosha; nalo: Blanketi dogo, hutaweza kujifunika. Kwani Bwana atainuka kama kwenye mlima wa Perasimu, achafuke kama kule bondeni karibu ya Gibeoni, aifanye kazi yake, nayo hiyo kazi yake ni ngeni, atumike katika matumishi yake, nayo hayo matumishi yake hayajasikiwa bado. Sasa acheni kufyoza, vifungo vyenu visikazwe, kwani nchi zote zimekwisha kukatiwa shauri la angamizo, kama nilivyosikia kwa Bwana Mungu aliye Mwenye vikosi. Sikilizeni, mwisikie sauti yangu! Angalieni, mlisikie neno langu! Inakuwaje? Mlima hulima siku zote, apate kumwaga mbegu? Au huponda siku zote madongo na kupalinganya? Au sivyo: alipokwisha kuusawasawisha mchanga wa juu, humwaga mbegu za maboga na za pilipili, nazo huzitupatupa, kisha hupanda nazo ngano nzuri mistarimistari, hata mtama na mahindi, nao uwele kandokando? Hivyo Mungu wake alimfundisha yafaayo na kumwonyesha. Kwani mbegu za maboga hazipurwi kwa magogo, mbegu za pilipili hazipitwi juu na magurudumu ya magari, ila mbegu za maboga zinafikichwa kwa vijiti, pilipili vilevile zinapigwapigwa kwa fimbo. Je? Ngano zinapondwa? Hapana, hawazipuri pasipo kukoma; hata wakipitisha magari na farasi wao, hawazipondi. Hayo nayo yalitoka kwake Bwana Mwenye vikosi, mizungu yake hustaajabisha, utambuzi wake ni mkuu. Umekwisha kuapizwa, wewe Simba wa Mungu! Wewe Simba wa Mungu! Wewe mji, Dawidi alimotua! Ongezeni mwaka kwa mwaka na kula sikukuu miaka mizima! Kisha nitamsonga Simba wa Mungu, kuweko kipiga kite na kuugua; ndipo, atakapokuwa mbele yangu Simba wa Mungu wa kweli. Ndipo, nitakapokupigia makambi, yakuzinge, kisha nitakujengea boma la kukusonga, nitaisimamisha hata minara, nipate kukushinda. Hapo ndipo, utakaponyenyekea, useme na kulala chini, maneno yako, utakayonitolea toka mavumbini, yatakuwa ya kujipunguza, sauti yako itakuwa kama ya mzimu atokaye kuzimuni, maneno yako ya kusema uvumbini yatakuwa ya kunong'ona tu. Lakini mavumo ya wale wageni waliokujia yatakuwa kama mavumbi membamba, kweli mavumo ya hao wakorofi yatakuwa kama makapi yapeperushwayo; nayo yatakuwa kwa ghafula, wagunduliwe nayo. Maana utakaguliwa na Bwana Mwenye vikosi, atakapokujia na kuitetemesha nchi kwa ngurumo, kwani ni mwenye sauti kuu, ataleta nao upepo wa kimbunga ulio wenye nguvu na ndimi za moto ulao. Yatakuwa kama ndoto, mtu aliyoiota usiku, hayo mavumo ya wamizimu waliokuja kumshambulia Simba wa Mungu nao waliolipigia boma lake vita na kumsonga. Itakuwa kama mwenye njaa anayeota akila chakula, lakini anapoamka hakuna kitu kwake, au kama mwenye kiu anayeota akinywa, lakini anapoamka hutweta na kuivuta roho yake. Hivyo ndivyo, yatakavyokuwa mavumo ya wamizimu wote, waliokuja kuushambulia mlima wa Sioni! Tumbueni macho na kuyakodoa! Yatieni giza na kupofuka! Wamelewa, lakini si kwa mvinyo, wanapepesuka, lakini si kwa kileo. Kwani Bwana amewamwagia ninyi roho ya usingizi mwingi, akayafumba macho yenu, ninyi wafumbuaji, akavifunika vichwa vyenu, ninyi wachunguzaji. Hayo yote mliyoyaona yakawa kwenu kama maneno ya kitabu kulichofungwa na kutiwa muhuri; kama ajuaye kusoma anapewa na kuambiwa: Kisome hiki! atajibu: Siwezi, kwani kimefungwa na kutiwa muhuri. Kama asiyejua kusoma anapewa na kuambiwa: Kisome hiki! atajibu: Sijui kusoma. Bwana akasema: Ukoo huu hunikaribia na vinywa vyao, huniheshimu kwa midomo tu, lakini mioyo yao inanikalia mbali; kwa sababu hii hunicha bure, kwani hufundisha mafundisho yaliyo maagizo ya watu tu. Kwa hiyo na mwone, ninavyoendelea kuufanyizia ukoo huu mambo ya mataajabu na ya vioja, werevu wao walio werevu wa kweli kwao upotee, nao utambuzi wa watambuzi wao usionekane. Yatawapata wao walao njama, kwamba: wamfiche Bwana mashauri yao! Nao wafanyao gizani kazi zao na kusema: Yuko nani anayetuona? Yuko nani anayetujua? Mmepotea kabisa! Uko udongo unaowaziwa kuwa sawa na mfinyanzi? Au kiko kiumbe kiwezacho kumwambia aliyekiumba: Hukunifanya? Au kiko chombo kiwezacho kumwambia aliyekifinyanga: Hujui kitu? Sicho kitambo kidogo bado, Libanoni kugeuke kuwa shamba, nayo mashamba yawaziwe kuwa mwitu? *Siku ile viziwi watayasikia maneno yaliyoandikwa, nayo macho ya vipofu yaliyokuwa yenye giza jeusi yataona. Nao wanyonge wataendelea kumfurahia Bwana nao walio wakiwa kuliko watu wengine watamshangilia Mtakatifu wa Isiraeli. Kwani wakorofi watakuwa wamekwisha, nao wafyozaji watakuwa wameangamia, nao wote watakuwa wameng'olewa waliokataa kulala usingizi, wapate kuwapotoa wenzao. Ndio wanaokosesha wengine shaurini, ndio wanaowategea waamuliao penye malango ya mji, kwani hivyo wanawapotoa waongofu, wasishinde shaurini.* Kwa sababu hii Bwana alimkomboa Aburahamu, akauambia mlango wa Yakobo: Sasa Yakobo hatapatwa tena na soni, wala uso wake hautamvilia tena. Kwani watoto wake watakapoona, mikono yangu itakayoyafanya kwao, watalitakasa Jina langu, ndiko kumtakasa Mtakatifu wa Yakobo na kumcha Mungu wa Isiraeli. Ndipo, waliopotea rohoni watakapojua utambuzi nao walionung'unika watajifundisha yafaayo. Ndivyo, asemavyo Bwana: Yatawapata wale wana wabishi wapigao shauri lisilo la kwangu, wafanyao agano pasipo Roho yangu, kusudi waongeze kosa kwa kosa. Ndio wanaokwenda kushuka Misri pasipo kukiuliza kinywa changu, wajipatie nguvu kwa nguvu za Farao kwa kukikimbilia kivuli cha Misri. Lakini nguvu zake Farao zitawageukia, ziwatie soni, nako kukikimbilia kivuli cha Misri kutawapatia matusi. Ijapo wakuu wake waje Soani, ijapo wajumbe wake wafike mpaka Hanesi, wao wote wataona soni na watu wasiowafalia kitu, kwa kuwa hawawezi kuwasaidia au kuwapatia cho chote kuwafaliacho, kwani wanawatia soni tu, wengine wawabeze na kuwatukana. Tamko zito lililotoka kwa ajili ya nyama wa kusini: Wanapita katika nchi yenye masongano na mahangaiko, kwani wamo simba na chui, pili na nyoka za moto warukao. Huko wanapitisha mali zao migongoni kwa punda, nako kwenye nundu za ngamia malimbiko yao, wayapelekee watu wasiowafalia kitu. Nayo Misri msaada wake ni kama mvuke, ni wa bure tu, kwa sababu hii waliipa jina hili: Mkuu wa maneno anayejikalia tu. Sasa nenda, uyachore katika kibao machoni pao, kisha uyaandike namo kitabuni, siku za nyuma yapate kuwashuhudia kale na kale. Kwani ndio watu wabishi na wana wenye uwongo, kweli ndio wana wasiotaka kuyasikia Maonyo ya Bwana. Huwaambia waonaji: Msione! nao watazamaji: Msitutazamie yaliyo ya kweli! Sharti mtuambie yaliyo mafuta ya midomo, sharti mtutazamie madanganyifu! Ondokeni njiani penye kweli! Ipotoeni mikondo inyokayo! Tuacheni, tupumzike, tusimwone Mtakatifu wa Isiraeli! Kwa hiyo Mtakatifu wa Isiraeli anasema: Kwa kuwa mmelikataa neno hili, mkayaegemea mambo yenye ukorofi na upotovu, mkayatumia ya kujishikizia: kwa sababu hii hizo manza, mlizozikora, zitakuwa kama ufa unaokwenda ukipanuka katika ukuta mrefu, nao utabomoka ghafula na kuwagundua watu. Naye Bwana atauvunja, kama watu wanavyovunja mtungi wakiupigapiga pasipo kuuhurumia, hapo, utakapovunjika, kisipatikane kigae cha kupalia moto jikoni, wala cha kutekea maji kisimani. Kwani hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu, aliye Mtakatifu wa Isiraeli: Mtakaporudi na kutulia, mtaokolewa; mtakaponyamaza na kujiegemeza, mtapata nguvu, lakini mmekataa! Mkasema: Hapana! Na tupande farasi, tupige mbio! Kwa hiyo mtakimbia. Mkasema: Na tupande farasi wenye mbio sana! Kwa hiyo watakaowafukuza watawapigisha mbio. Elfu wa kwenu wataikimbia yowe ya mmoja; watano wakipiga yowe, mtakimbia wote, mpaka masao yenu yawe kama mlingoti ulioko mlimani juu au kama bendera iliyoko kilimani. Kwa hiyo Bwana anangoja, apate kuwatolea upole; kwa hiyo anainuka, apate kuwahurumia, kwani Bwana ni Mungu wa kuamua kweli; wenye shangwe ni wote wanaomngoja, kwani walio wa Sioni watakaa Yerusalemu. Hamtalia machozi kamwe, atawaendea kwa upole; atakapozisikia sauti za vilio vyenu atawaitikia. Kweli, Bwana amewalisha mikate ya masongano, akawanywesha maji ya mahangaiko, lakini wafunzi wako hawatajificha tena, ila macho yako yatakuwa yakiwatazamia wafunzi wako. Nayo masikio yako yatasikia neno litokalo nyuma yako kwamba: Njia ni hii, ishikeni! kama mtakuwa mmeiacha kuumeni au kushotoni. Hapo ndipo, mtakapovichafua vinyago vyenu vya miti vilivyofunikwa na fedha navyo vilivyofunikwa na dhahabu, utavitupatupa, kama ni takataka, na kuviambia: Tokeni kwetu! Naye atakupa mvua za mbegu zako, ulizozipanda shambani, nalo shamba litakutolea mikate itakayokuwa yenye nguvu ya kunonesha, nao kondoo wako watalisha siku zile kwenye uwanda mpana. Nao ng'ombe na punda wako wanaolima shamba watakula muhindi ulioungwa na majani yenye chumvi, nao utakuwa umepepetwa kwa ungo na kipepeto. Katika kila mlima mrefu, hata katika kila kilima kiendacho juu kutakuwa na vijito vya maji yarukayo; itakuwa siku ile, wengi watakapouawa, minara itakapoanguka. Nao mwanga wa mwezi utakuwa kama wa jua, nao mwanga wa jua utaongezeka mara saba, uwe kama wa siku saba. Itakuwa siku ile, Bwana atakapovifunga vidonda vyao walio ukoo wake na kuyaponya machubuko, aliyowapiga. Tazameni, Jina la Bwana linakuja toka mbali, makali yake yanawaka, moshi mwingi unapanda, midomo yake imejaa machafuko, ulimi wake ni kama moto ulao! Pumzi yake ni kama mto udidimizao, nayo maji yake hufika shingoni, awapepete wamizimu katika pepeto liangamizalo, atie mataifa mazima hatamu vinywani za kuwapoteza. Nanyi mtaimba, kama watu wanavyoimba katika usiku wa kuandalia sikukuu, mtafurahi mioyoni kama wasafiri wanaokwenda na kupiga mazomari, waje mlimani kwa Bwana aliye mwamba wa Isiraeli. Ndipo, Bwana atakapoipaza sauti yake yenye utukufu, atauonyesha nao mkono wake, jinsi unavyokunjuka, akifoka kwa ukali na kuwakisha ndimi za moto ulao, akileta kimbunga na mvua yenye maji mengi pamoja na mvua ya mawe. Kwani Waasuri watastushwa na sauti yake Bwana, atakapowapiga kwa fimbo yake: kila mara fimbo ya kuwapiga itakapotokea, Bwana akiielekeza, iwajie, itakuwa kwa kupiga patu na mazeze, vita vyake vitakuwa hivyo akiwatisha na kuwapigapiga. Kwani tangu kale pametengenezwa mahali pa kuchinjia watu, wawe ng'ombe za tambiko, naye mfalme amepatengenezewa pake, napo ni papana na parefu kwenda chini; kuzunguka hapo moto uko tayari, hata kuni nyingi zimekwisha kupangwa; pumzi ya Bwana yenye moto wa kiberitiberiti itaziwasha. Yatawapata washukao kwenda Misri kutafuta msaada, wakijishikiza kwa farasi, wakaegemea magari, kwamba ni mengi, hata wapanda farasi, kwamba ni wenye nguvu sana, lakini hawakumtazamia Mtakatifu wa Isiraeli, Bwana hawakumtafuta. Naye ni mwenye werevu wa kweli; kwa hiyo analeta kibaya, nayo maneno yake hayaondoi: nyumba zao wafanyao mabaya ataziinukia, vilevile msaada wao wafanyao maovu. Misri ndio watu tu, sio Mungu; farasi wao ndio nyama, sio roho. Bwana akiukunjua mkono wake, ndipo, huyo mwenye kusaidia anapojikwaa, ndipo, naye mwenye kusaidiwa anapoanguka, wakaanguka wote pamoja. Kwani hivi ndivyo, Bwana alivyoniambia: Itakuwa kama simba au mwana wa simba, akikamata kondoo na kunguruma; kisha wachungaji wakiitana wengi, wamnyang'anye, hazistukii sauti zao, wala hatishiki kwa makelele yao; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi atakavyoshuka kupiga vita, mlimani kwa Sioni nako kwenye kilima chake. Bwana Mwenye vikosi ataukingia Yerusalemu kama ndege warukao, kwa kukinga atawaponya, kwa kuwapita atawakomboa. Rudini kwake yeye, mliyemwacha kabisa, ninyi wana wa Isiraeli! Kwani siku ile kila mtu atavikataa vinyago vyake vya fedha na vinyago vyake vya dhahabu, mlivyojitengenezea kwa mikono yenu, vikawakosesha. Ndipo, Waasuri watakapouawa kwa panga zisizo za waume, kweli panga zitawala, lakini sizo za watu; hizo panga watazikimbia, nao vijana wao watakuwa watumwa. Naye aliyekuwa mwamba wao atakimbia kwa woga, nao walio wakuu wao watazimia kwa kuona bendera. Ndivyo, asemavyo Bwana alioko Sioni na moto wake alioko na jiko lake huko Yerusalemu. Na mwone, mfalme akitawala kwa wongofu, wakuu nao wakiwaendea watu kwa unyofu! Kila mmoja wao atakuwa kimbilio penye kimbunga na ficho penye mvua nyingi, watakuwa kama vijito vya maji katika nchi kavu, na kama kivuli cha mwamba mkuu katika nchi inayotwetesha. Hapo macho yao waonao hayatazibana tena, nayo masikio yao wasikiao yatasikiliza. Nayo mioyo yao walio wa juujuu itatambua na kujua maana, nazo ndimi zao wagugumizao maneno zitasema upesi maneno ya sawasawa. Mjinga hataitwa tena bwana mkubwa, wala mdanganyifu hataambiwa tena kuwa mkuu. Kwani mjinga husema yenye ujinga, nao moyo wake hufanya maovu: hufanya yaliyo machafu machoni pake Bwana, tena husema maneno ya kupoteza watu, wasimjie Bwana, mwenye njaa humwacha, akae vivyo hivyo na njaa yake, naye mwenye kiu humnyima cha kunywa. Naye mdanganyifu mizungu yake ni mibaya: huwaza njia za kupotoa, apate kuangamiza wanyonge kwa maneno ya uwongo, ijapo mkiwa aseme yanyokayo shaurini. Lakini aliye bwana mkubwa huwaza yapatanayo na ubwana, naye atayasimamia ya ubwana. Ninyi wanawake msiojisumbua, inukeni, mwisikilize sauti yangu! Nanyi wanawali mnaojikalia tu, yasikilizeni maneno yangu! Siku za nyuma, mwaka utakapopita, mtatetemeka nyinyi mnaojikalia tu, kwani mavuno ya zabibu yatakuwa yametoweka, nayo mavuno ya matunda hayatakuwa tena. Stukeni, ninyi msiojisumbua! Tetemekeni, ninyi mnaojikalia tu! Jivueni na kuondoa mavazi, mpate kujifunga viunoni tu. Jipigeni vifua kwa ajili ya mashamba yaliyokuwa yakipendeza, na kwa ajili ya mizabibu iliyokuwa ikizaa sana! hata kwa ajili ya nchi yao walio ukoo wangu, kwani miti yenye miiba kama mikunju itakuwamo; hata kwa ajili ya nyumba zote za furaha na kwa ajili ya huo mji uliojaa vigelegele. Kwani majumba yatakuwa mahame, makelele ya mjini yatakuwa yameachwa, boma lake na minara yake itakuwa imegeuka kuwa mapango kale na kale ya kufurahisha vihongwe na malisho ya makundi ya kondoo na mbuzi. Itakuwa hivyo, mpaka tutakapomwagiwa Roho itokayo juu. Ndipo, nyika itakapokuwa shamba la mizabibu, nalo shamba la mizabibu litawaziwa kuwa mwitu; ndipo, mashauri ya nyikani yatakapokatwa kwa unyofu, nao wongofu utakaa mashambani kwa mizabibu. Nayo kazi ya wongofu itakuwa kuleta utengemano, nao utumishi wa wongofu utakuwa kuwapatia watu utulivu, wakae salama kale na kale. Ndipo, wao walio ukoo wangu watakapokaa mahali penye utengemano na katika makao ya kukaa salama na katika vituo visivyowasumbua. Lakini kwanza mvua ya mawe inye ya kuvunja mwitu, tena ya kuunyenyekeza mji unyenyekee kabisa. Ninyi mtakuwa wenye shangwe, kwa kuwa mtapanda kandokando ya maji po pote, mtawaacha ng'ombe na punda, wajiendee, wanapotaka. Mwenye kuapizwa ni wewe mkorofi usiyekorofishwa bado, mwenye kuapizwa ni wewe mpokonyi usiyepokonywa bado. Utakapomaliza kukorofisha utakorofishwa, utakapomaliza kupokonya utapokonywa! Bwana, tuwie mpole! Wewe tumekungojea; uwe mkono wao kila kunapokucha! Uwe nao wokovu wetu, tunaposongeka! Waliposikia sauti ya uvumi, makabila ya watu yalikimbia, wewe ukiinuka, wamizimu hutawanyika. Ndipo, mateka yenu yatakapookotwa, kama watu wanavyookota nzige; kama funutu wanavyojikimbilia, ndivyo, watakavyojikimbilia. Bwana ametukuka, kwani anakaa juu, hujaza Sioni maamuzi yaongokayo. Ndipo, siku zako zitakapokuwa zimeelekea pamoja, yenye werevu wa kweli na utambuzi yatakuwa malimbiko ya kujisaidia, kumwogopa Bwana ndiko kutakakokuwa mali zake Sioni. Wasikilizeni wanguvu wao wanaopiga makelele huko nje, wajumbe wa kuomba utengemano wanalia kwa uchungu. Barabara ziko peke yao, hakuna apitaye njiani. Amevunja agano kwa kuibeza miji na kwa kuwawazia watu kuwa si kitu. Nchi inazimia kwa kusikitika: Libanoni kumekauka kwa kuona soni, Saroni kumegeuka kuwa kama nyika, Basani na Karmeli kumepakatika majani. Ndivyo, anavyosema Bwana: Sasa nitainuka, sasa nitajitukuza, sasa nitaoneka. Kwa kuwa mimba zenu ni za majani makavu, mtazaa mabua makavu tu; kufoka kwenu ni moto utakaowala wenyewe. Ndipo, makabila ya watu yatakapochomwa kama chokaa, watakuwa kama miiba iliyokatwa ya kuteketezwa na moto. Sikieni, ninyi mkaao mbali, mliyoyafanya! nanyi mkaao karibu, zijueni nguvu zangu! Wakosaji walioko Sioni wamestuka, tetemeko likawashika wapotovu, wakasema: Kwetu sisi yuko nani awezaye kukaa penye moto ulao? Kwetu sisi yuko nani awezaye kukaa penye majiko yasiyozima kale na kale? Ni yeye aendeleaye kwa wongofu naye asemaye yanyokayo, naye akataaye mapato ya ukorofi naye akung'utaye mikono yake, isishike mapenyezo, naye ayazibaye masikio yake, asisikie mashauri ya damu zilizomwagwa, naye ayafumbaye macho yake, asiyaone mabaya. Ndiye atakayekaa juu: maboma yaliyoko magengeni yatakuwa ngome yake, mkate atapewa tu, nayo maji yake hayatakauka. Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataiona nayo nchi, jinsi itakavyopanuka. Moyo wako utakapoyawaza yale mastusho utasema: Yuko wapi mwenye kuhesabu fedha? Yuko wapi mwenye kuzipima? Yuko wapi mwenye kuihesabu minara? Lile kabila lenye ukorofi hulioni tena, ndimi zao zikagugumiza tu maneno yasiyokuwa na maana. Utazameni Sioni ule mji wetu wa kukusanyikiamo! Macho yako yataona, ya kuwa Yerusalemu ni kao lisilosumbua, ni hema lisilosafiri, mambo zake hazing'olewi kale na kale, kamba zake zote hazikatiki kamwe. Kwani huko Bwana mwenye utukufu atakuwa kwetu, atukingie penye mito mikubwa yenye mikono mipana, mitumbwi ya kuvukia haitapatikana, wala vyombo havitapita hapo. Kwani Bwana ni mwamuzi wetu, Bwana ndiye atakayetuongoza, Bwana ni mfalme wetu, yeye ndiye atakayetuokoa. Kamba zako zilikuwa zimelegea, hazikuukaza ulingo wa mlingoti wao, wala hazikutanda tanga; ndipo, mateka mengi mazuri yatakapogawanywa, nao waendao pecha wataweza kujitwalia mateka. Hapataonekana mwenyeji atakayesema: Nimeugua, kwani watu watakaokaa mle watakuwa wameondolewa manza, walizozikora. Karibuni, ninyi wamizimu, msikie! Nanyi makabila ya watu, angalieni! Nchi na isikilize nayo yote yaliyoko! Nao ulimwengu nayo yote yachipukako! Kwani Bwana amewachafukia wamizimu wote, makali yake yawatokee vikosi vyao vyote; akawatia mwiko, wasiwepo tena, akawatoa, wachinjwe. Watakaouawa kwao watatupwa tu, mnuko wa mizoga yao utaenea, nayo milima italegezwa kwa damu zao. Hata vikosi vyote vya mbinguni vitayeyuka, nazo mbingu zitazingwa kama kizingo cha karatasi, vikosi vyake vyote vitanyauka, kama majani yanavyonyauka kwenye mizabibu nako kwenye mikuyu. Kwani upanga wangu ukilewa mbinguni, mtauona, unavyowashukia Waedomu; nimewatia mwiko wa kuwapo, wapatilizwe. Bwana yuko na upanga uliojaa damu, ukapakwa mafuta: ni damu za wana kondoo na za madume, ni mafuta ya mafigo ya madume; kwani iko sikukuu ya tambiko ya Bwana huko Bosira, liko chinjo kubwa katika nchi ya Edomu. Pamoja nao hata nyati wataanguka, nayo madume na manono ya ng'ombe, nchi yao italewa kwa kuzinywa damu zao, nao mchanga utapata nguvu kwa mafuta yao. Kwani hiyo ni siku ya Bwana ya kulipiza, ni mwaka wa kuvilipisha vita, walivyoupelekea Sioni. Mito yake itageuzwa kuwa lami, nayo mavumbi yake yatakuwa viberiti, hivyo nchi yao itakuwa lami iwakayo moto. Usiku na mchana hautazima, moshi wake utapanda kale na kale; kwa vizazi na vizazi itakuwa jangwa, siku zote za kale na kale hapataonekana atakayepapita. Watakaoitwaa ni korwa na nungu, hata mabundi na makunguru watakaa huko; Bwana atatanda juu yake kamba ya kuipimia, iwe peke yake, ataweka nayo mawe ya kuipimia, iwe tupu kabisa. Hakuna wakuu wake watakaoiita kuwa nchi ya kifalme, wote walioitawala watakuwa wametoweka. Miti yenye miiba itamea majumbani mwao, namo mabomani viwawi na mangugi; namo ndimo, watakaamo mbweha na mbuni. Huko vimburu watakutana na mbwa wa mwitu, shetani atamwita shetani mwenziwe; tena ndiko, mzuka wa kike wa usiku utakakotua na kujipatia pa kupumzikia. Naye nyoka wa mamba atatengeneza kuko shimo lake, atage mayai, apate watoto, awatunze kuvulini pake, Tena ndiko, mwewe watakakokusanyikana, kila mmoja na mwenziwe. Tafuteni katika kitabu cha Bwana, msome! Hawa nyama hakuna hata mmoja wao asiyepatikana, wote hakuna hata mmoja amkosaye mwenziwe; kwani kinywa chake mwenyewe ndicho kilichowaagiza, nayo Roho yake ndiyo inayowakusanya. Yeye ndiye aliyewapigia kura, nao mkono wake ndio uliowagawia mafungu yao, naye aliyapima kwa kamba ya kupimia, wayatwae, yawe yao ya kale na kale, wakae huko vizazi na vizazi. Nyika na nchi kavu, na mchangamke, nalo jangwa na lipige vigelegele kwa kuchipuka na kuchanua kama shamba la maua ya uwago. Litachipuka kweli na kuchanua, lipige vigelegele na shangwe, litapewa utukufu wa Libanoni na urembo wa Karmeli nao wa Saroni; hao watauona utukufu wa Bwana na urembo wa Mungu wetu. *Mikono iliyolegea itieni nguvu! Nayo magoti yaliyojikwaa yashupazeni! Waambieni waliopotelewa na mioyo: Jipeni mioyo, msiogope! Mtazameni Mungu wenu! Lipizi linakuja, wanalipishwa na Mungu; yeye ndiye atakayewaokoa ninyi. Hapo ndipo, yatakapofumbuliwa macho ya vipofu, ndipo, yatakapozibuliwa masikio ya viziwi, ndipo, viwete watakaporukaruka kama kulungu, ndipo, ndimi za mabubu zitakapopiga shangwe, kwani maji yatabubujika nyikani, nayo mito jangwani. Mchanga wenye moto utageuka kuwa ziwa, nayo nchi iliyokufa kwa kiu itatoka visima vya maji. Penye makao na matuo ya mbweha pataota nyasi na matete na magugu. Hata barabara iliyotengenezwa vizuri itakuwako, nayo itaitwa Njia Takatifu; mwenye machafu hataishika, ila itakuwa yao tu, watakaoishika ya kukuendeako, nao wajinga hawatapotelewa nayo. Simba hatakuwako kule, wala nyama wakali wengine hawatakupanda, hawataonekana huko kabisa. Hivyo wale waliokombolewa wataendelea kuishika. Waliookolewa na Bwana watarudi, waje Sioni na kupiga shangwe, furaha za kale na kale zitawakalia vichwani pao, machangamko na furaha zitawafikia, lakini machungu yatakimbia, wasipige kite tena.* Ikawa katika mwaka wa 14 wa mfalme Hizikia, ndipo, Saniheribu, mfalme wa Asuri, alipoipandia miji yote ya Wayuda iliyokuwa na maboma, akaiteka. Kisha mfalme wa Asuri akamtuma mkuu wa askari, atoke Lakisi kwenda Yerusalemu na kikosi kikubwa kwake mfalme Hizikia. Akaja kusimama kwenye mfereji wa ziwa la juu katika barabara iendayo Shambani kwa Dobi. Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme, na Sebuna aliyekuwa mwandishi na Yoa, mwana wa Asafu, aliyekuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa wakamtokea. Mkuu wa askari akawaambia: Mwambieni Hizikia: Hivi ndivyo, mfalme mkuu, mfalme wa Asuri, anavyosema: Hilo egemeo, unaloliegemea, ndio nini? Nasema: Ni maneno ya midomo tu, ukisema: Nimekata shauri na kujipa moyo wa kupiga vita. Sasa unamwegemea nani, ukinikataa na kuacha kunitii? Tazama! Egemeo lako, unaloliegemea, ni Misri, hilo fimbo la utete unyongekao! Mtu akilikongojea, litamwingia kiganjani, limchome. Ndivyo, Farao, mfalme wa Misri, anavyowawia wote waliomwegemea. Ukiniambia: Tunamwegemea Bwana Mungu wetu, basi, yeye siye, ambaye Hizikia aliwakataza watu kumtambikia vilimani pake napo penye meza zake za kutambikia, alipowaambia Wayuda na Wayerusalemu: Sharti mmwangukie mbele ya meza hii tu ya kumtambikia? Sasa na upinge na bwana wangu, mfalme wa Asuri: Nitakupa farasi 2000, kama wewe unaweza kujipatia watu wa kuwapanda. Usipowapata utawezaje kuuelekeza nyuma uso wa mwenye amri mmoja tu, ijapo awe mdogo katika watumishi wa bwana wangu? Tena unawaegemea Wamisri, kwa kuwa wako na magari na wapanda farasi. Bwana alikuwa hayuko, nilipoipandia sasa nchi hii, niiangamize? Bwana ndiye aliyeniambia: Ipandie nchi hii, uiangamize! Ndipo, Eliakimu na Sebuna na Yoa walipomwambia mkuu wa askari: Sema Kishami na watumishi wako! Kwani tunakisikia; usiseme na sisi Kiyuda masikioni pa watu hawa walioko ukutani! Mkuu wa askari akawajibu: Je? Bwana wangu amenituma kwa bwana wako na kwako kuyasema haya maneno? Sio kwa watu hawa wanaokaa ukutani watakaokula pamoja nanyi mavi yao na kunywa mikojo yao? Kisha mkuu wa askari akatokea, akapaza sauti sana na kusema Kiyuda kwamba: Yasikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Asuri! Hivi ndivyo, mfalme anavyosema: Hizikia asiwadanganye! Kwani hataweza kuwaponya ninyi. Wala Hizikia asiwaegemeze Bwana kwamba: Bwana ndiye atakayetuponya, mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Asuri. Msimwitikie Hizikia! Kwani hivi ndivyo, mfalme wa Asuri anavyosema: Fanyeni na mimi maagano ya mbaraka, mje kunitokea, mpate kula kila mtu mazao ya mzabibu wake na ya mkuyu wake, mpate kunywa kila mtu maji ya shimo lake mwenyewe, mpaka nitakapokuja, miwachukue kuwapeleka katika nchi iliyo kama nchi yenu. Nayo ni nchi inayojaa ngano na pombe, ni nchi yenye vyakula na mizabibu. Hizikia asiwapoteze na kusema: Bwana atatuponya! Je? Miungu ya wamizimu iliweza mmoja tu kuiponya nchi yake, isichukuliwe na mfalme wa Asuri? Ilikuwa wapi miungu ya Hamati na ya Arpadi? Ilikuwa wapi miungu ya Sefarwaimu? Hata Samaria haikuweza kuiponya, nisiichukue! Katika miungu yote ya nchi hizi ni ipi iliyoweza kuziponya nchi zao, nisizichukue? Basi, Bwana atawezaje kuuponya Yerusalemu, nisiuchukue? Wakanyamaza, hawakumjibu neno, kwani mfalme alikuwa amewaagiza kwamba: Msimjibu! Kisha Eliakimu, mwana wa Hilikia, aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme, na Sebuna aliyekuwa mwandishi na Yoa, mwana wa Asafu, aliyekuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa wakaja kwa Hizikia wenye nguo zilizoraluliwa, wakamsimulia maneno ya mkuu wa askari. Ikawa, mfalme Hizikia alipoyasikia, akazirarua nguo zake, akajifunga gunia, akaingia Nyumbani mwa Bwana. Akamtuma Eliakimu aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme na Sebuna aliyekuwa mwandishi na watambikaji wazee waliokuwa wamejifunga magunia kwenda kwa mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi. Wakamwambia: Hivi ndivyo, Hizikia anavyosema: Siku hii ya leo ni siku ya kusongwa na ya kupatilizwa na ya kutupwa, kwani watoto wamefikisha kuzaliwa, lakini nguvu za kuwazaa haziko. Labda Bwana Mungu wako ameyasikia yale maneno ya mkuu wa askari, ambayo bwana wake, mfalme wa Asuri, alimtuma kumbeua Mungu Mwenye uzima kwa kuyasema; Bwana Mungu wako na ampatilizie yale maneno, aliyoyasikia! Nawe na uje kuwaombea waliosalia walioko bado! Wakaja hao watumishi wa mfalme Hizikia kwake Yesaya. Yesaya akawaambia: Mwambieni bwana wenu hivi: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Usiyaogope yale maneno, uliyoyasikia, vijana wa mfalme wa Asuri waliyonitukana nayo! Utaniona, nikimtia roho nyingine, asikie habari, kisha arudi katika nchi ya kwao, nako huko kwao nitamwangusha kwa upanga. Mkuu wa askari aliporudi akamkuta mfalme wa Asuri, akipiga vita Libuna, kwani alisikia, ya kuwa mfalme ameondoka Lakisi. Huko mfalme akasikia habari ya Tirihaka, mfalme wa Nubi, kwamba: Tazama, ametoka kukupelekea vita! Ndipo, alipotuma wajumbe kwake Hizikia kwamba: Hivyo mtamwambia Hizikia, mfalme wa Yuda, mkisema: Asikudanganye Mungu wako, wewe umwegemeaye kwamba: Yerusalemu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Asuri. Kumbuka, uliyoyasikia mwenyewe, wafalme wa Asuri waliyozifanyizia nchi zote wakiziangamiza na kuzitia mwiko wa kuwapo! Nawe utapona? Je? Miungu ya wamizimu iliwaponya, baba zangu walipowamaliza, wale watu wa Gozani na wa Harani na wa Resefu nao wana wa Edeni walioko Tilasari? Yuko wapi mfalme wa Hamati, naye mfalme wa Arpadi, naye mfalme wa mji wa Sefarwaimu, naye wa Hena, naye wa Iwa? Hizikia alipozichukua barua hizo mikononi mwa wajumbe, akazisoma; kisha akapanda kwenda Nyumbani mwa Bwana. Humo Hizikia akazizingua mbele yake Bwana, kisha Hizikia akamlalamikia Bwana akisema: Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, uyakaliaye Makerubi, wewe ndiwe Mungu peke yako wa nchi zote za kifalme, wewe ndiwe uliyezifanya mbingu na nchi. Bwana, litege sikio lako, usikie! Bwana, yafumbue macho yako, uone! Yasikie haya maneno yote ya Saniheribu, aliyoyatuma, akubeue uliye Mungu Mwenye uzima! Ni kweli, Bwana, wafalme wa Asuri wameziangamiza zile nchi zote na mashamba yao, wakaitupa miungu yao motoni, kwani hiyo siyo miungu, ila ni kazi za mikono ya watu, ni miti na mawe tu, kwa hiyo waliweza kuiharibu. Bwana Mungu wetu, tuokoe sasa mkononi mwake! Ndipo, nchi zote za kifalme zitakapojua, ya kuwa wewe ndiwe Bwana peke yako. Ndipo, Yesaya, mwana wa Amosi, alipotuma kwake Hizikia kumwambia: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli, uliyemlalamikia kwa ajili ya Saniheribu, mfalme wa Asuri. Hili ndilo neno, Bwana alilolisema kwa ajili yake: Mwanamwali binti Sioni, amekubeza na kukufyoza; binti Yerusalemu, amekutingishia kichwa nyuma yako. Ni nani, uliyembeua na kumtukana? Ni nani, uliyempalizia sauti na kuyaelekeza macho yako juu? Ni Mtakatifu wa Isiraeli. Bwana ndiye, uliyembeua vinywani mwa watumishi wako ukisema: Kwa kuwa magari yangu ni mengi, nimepanda milimani juu huko ndani Libanoni, nikaikata miangati yake mirefu na mivinje yake iliyochaguliwa, nikafika kwake huko juu kileleni, msitu unakokuwa kama shamba lake la miti. Nilipochimba nikapata maji ya kunywa, tena nikaikausha mito yote ya Misri kwa nyayo za miguu yangu. Je? Hujasikia kwamba: Niliyoyafanya kale, niliyoyalinganisha siku za mbele, sasa nimeyaleta, yatimie; wewe ukawa wa kutowesha miji yenye maboma, iwe machungu ya mawe na mabomoko. Nao waliokaa humo mikono yao ikawa mifupi, wakastuka, wakaingiwa na soni, wakawa kama mapalizi ya shambani au kama ndago za uwandani au kama majani yameayo juu ya kipaa au kama shamba linyaukalo pasipo kuzaa. Ninakujua kukaa kwako na kutoka kwako na kuingia kwako; ninavijua navyo, unavyovikasirikia. Kwa sababu unanikasirikia, majivuno yako yakapanda kuingia masikioni mwangu, nitakutia pete yangu puani mwako, nayo hatamu yangu midomoni mwako, kisha nitakurudisha katika njia ileile, uliyokuja nayo. Hiki kitakuwa kielekezo chako, Hizikia: Mwaka huu mtakula yaliyojipanda yenyewe, mwaka wa pili mtakula yaliyoota mashinani, mwaka wa tatu mmwage mbegu, mvune. Nayo mizabibu mtapanda, myale matunda yao. Ndipo, masao yao waliopona wa mlango wa Yuda watakapotia mizizi chini, kisha watazaa matunda juu. Kwani Yerusalemu yatatokea masao, nako mlimani kwa Sioni watatokea waliopona. Wivu wake Bwana Mwenye vikosi utayafanya hayo. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya mfalme wa Asuri: Hatauingia mji huu, wala hatapiga humu mshale, wala hataukaribishia ngao, wala hataujengea boma la kuuzingia. Njia, aliyokuja nayo, ileile atarudi nayo. Lakini humu mjini hatamwingia; ndiyo, asemavyo Bwana. Nitaukingia mji huu, niuokoe kwa ajili yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi. Akatokea malaika wa Bwana, akapiga makambini kwa Waasuri watu 185000. Walipoamka asubuhi wakawaona hao wote, ya kuwa wamekufa, ni mizoga tu. Ndipo, Saniheribu, mfalme wa Asuri, alipoondoka, aende zake, akarudi kwao, akakaa Niniwe. Ikawa, alipoomba nyumbani mwa mungu wake Nisiroki, ndipo, wanawe, Adarameleki na Sareseri walipompiga kwa upanga, ksha wakaikimbilia nchi ya Ararati, naye mwanawe Esari-Hadoni akawa mfalme mahali pake. Siku zile Hizikia akaugua, kufa kukamjia karibu. Ndipo, mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi, alipokuja kwake, akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Yaliyo yako yaagizie walio wa mlango wako! Kwani wewe utakufa, hutarudi kuwa mzima tena. Hizikia akageuka na kuuelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema: E Bwana, na uukumbuke mwenendo, nilioufanya mbele yako kwa welekevu, nikayafanya kwa moyo wote mzima, yaliyo mema machoni pako. Kisha Hizikia akalia kilio kikubwa. Ndipo, neno la Bwana lilipomjia Yesaya kwamba: Nenda, umwambie Hizikia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa baba yako Dawidi anavyosema: Nimesikia kuomba kwako, nikayaona hayo machozi yako. Basi, siku zako nitaziongeza na kukupa tena miaka kumi na mitano. Namo mkononi mwake mfalme wa Asuri nitakuponya, hata mji huu, maana nitaukingia mji huu. Nacho hiki kitakuwa kielekezo chako kitokacho kwa Bwana cha kwamba: Bwana atalifanya neno hili, alilolisema. Tazama: kuvuli kilichoshuka penye saa ya jua ya Ahazi nitakirudisha nyuma vipande kumi! Kisha jua likarudi penye saa ya jua vipande kumi, lilivyokuwa limevishuka. Huu ndio wimbo, Hizikia, mfalme wa Yuda, aliouandika katika ugonjwa wake alipokuwa amepona: Mimi nilisema: Sasa, siku zangu zinapokuwa zimefika kati, sharti niingie malangoni mwa kuzimu! Nimenyang'anywa miaka yangu iliyosalia. Nilisema: Sitamwona Bwana tena, maana Bwana yuko katika nchi yao walio hai; huko kwao wakaao katika nchi ya vivuli sitapata kuona mtu tena. Kituo changu kimeng'olewa, kikachukuliwa kwangu kama hema la mchungaji; nimezizinga siku za maisha yangu kama mfuma nguo azikate penye nyuzi zinazozishika; mchana utakapokuwa haujawa usiku bado, utanitowesha. Nikalia mpaka asubuhi, maana aliivunja mifupa yangu sawasawa kama simba; mchana utakapokuwa haujawa usiku bado, utanitowesha. Nikalia kama kinega au mbayuwayu nikapiga kelele kama hua, macho yangu yakafifia kwa kutazama juu kwamba: Bwana ninakorofika! Nikomboe! Sasa nisemeje? Aliyoniambia, yeye ameyafanya. Nami nitaendelea na kutulia miaka yangu yote kwa ajili ya uchungu, roho yangu iliouona. Bwana! Kwa maneno kama hayo watu hupata uzima, nao uzima wa roho yangu umo humo; nami umeniponya na kunirudisha uzimani. Tazama! Uchungu uliokuwa kweli uchungu kwangu umenipatia utengemano! Kwa kunipenda wewe umeitoa roho yangu mle shimoni mwa kutoweka, kwani makosa yangu yote uliyatupa nyuma yako. Kwani kuzimuni siko, wanakokushukuru, wala waliokufa sio wanaokushangilia, wala walioshuka shimoni sio wanaoungojea welekevu wako. Aliye hai, kweli aliye hai ndiye atakayekushukuru kama mimi leo. Baba huwajulisha watoto mambo ya welekevu wako. Bwana ndiye aliyetaka kuniokoa; kwa hiyo na tumpigie mazeze na kumwimbia Nyumbani mwa Bwana siku zetu zote za kuwapo! Kisha Yesaya akasema, walete andazi la kuyu, waliweke juu ya jipu, apate kupona. Hizikia akasema: Kielekezo ni nini cha kwamba: Nitapanda tena kwenda nyumbani mwa Bwana? Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani, mfalme wa Babeli, akatuma barua na matunzo kwake Hizikia kwani alisikia ya kuwa aliugua, akapona. Hizikia akawafurahia, akawaonyesha nyumba ya kuwekea mali zake, mlimo na fedha na dhahabu na manukato na mafuta mazuri, nayo nyumba yote ya mata yake, nayo yote pia yaliyooneka katika vilimbiko vyake. Hakikuwako kitu, ambacho Hizikia hakuwaonyesha, wala nyumbani mwake, wala katika ufalme wake wote. Kisha mfumbuaji Yesaya akaja kwa mfalme Hizikia, akamwuliza: Waume hao wamesema nini? Wametoka wapi wakija kwako? Hizikia akajibu: Wametoka nchi ya mbali, wakaja kwangu toka Babeli. Akauliza: Wameona nini katika nyumba yako? Hizikia akajibu: Wameyaona yote yaliyomo nyumbani mwangu, hakuna kitu katika vilimbiko vyangu, ambacho sikuwaonyesha. Ndipo, Yesaya alipomwambia Hizikia: Sikia neno la Bwana Mwenye vikosi! Tazama! Ziko siku zitakazokuja, ndipo, yote yaliyomo nyumbani mwako, nayo yote, baba zako waliyoyalimbika hata siku hii ya leo, yatakapopelekwa Babeli, hakitasalia hata kimoja; ndivyo, Bwana anavyosema. Namo katika wanao wa kiume waliotoka mwilini mwako, uliowazaa mwenyewe, watachukuliwa wengine, watumikie jumbani mwa mfalme wa Babeli. Hizikia akamwambia Yesaya: Neno la Bwana, ulilolisema, ni jema, kwani alisema moyoni: Katika siku zangu utakuwako utengemano wa kweli. *Watulizeni mioyo! Watulizeni mioyo walio ukoo wangu! Ndivyo, Mungu wenu anavyosema. Wayerusalemu wapeni mioyo na kuwatangazia, ya kuwa utumishi wao wa vita umemalizika, ya kuwa manza zao, walizozikora, zimekwisha kulipwa, kwani mkono wa Bwana umewalipisha mara mbili makosa yao yote. Iko sauti ya mtu apigaye mbiu nyikani: Itengenezeni njia ya Bwana! Yanyosheni nyikani mapito ya Mungu wetu! Vibonde vyote vifukiwe, navyo vilima vyote na vichuguu vyote vichimbuliwe! Napo palipopotoka panyoshwe, napo penye mashimo pawe njia ya sawasawa! Utukufu wake Bwana upate kufunuliwa, wote wenye miili wauone pamoja! Kwani kinywa chake Bwana kimevisema. Iko sauti ya mtu asemaye: Tangaza! Mwingine akasema: Na nitangaze nini? Kila mwenye mwili ni kama majani, nao uzuri wake wote ni kama ua la shambaani. Majani hunyauka, nayo maua hupukutika, upepo wa Bwana ukiyapuzia; kweli watu ndio majani. Majani hunyauka, nayo maua hupukutika, lakini Neno lake Mungu wetu litasimama kale na kale.* Jipandie mlima mrefu, Sioni, upige mbiu njema! Paza sauti na nguvu, Yerusalemu, upige mbiu njema! Paza sauti, usiogope! Iambie miji ya Yuda: Mtazameni Mungu wenu! Tazameni! Bwana Mungu anakuja mwenye nguvu! Mkono wake unamtengenezea ufalme. Tazama! Mshahara wake wa kulipa anao. nayo mapato yake yako mbele yake. Kama mchungaji anavyolichunga kundi lake, atawakusanya wana kondoo kwa mkono wake, awabebe kifuani, nao wanyonyeshao atawapeleka polepole. Yuko nani apimaye bahari kwa kofi lake? Yuko nani azilinganyaye mbingu kwa upana wa shibiri? Yuko nani aenezaye mavumbi ya nchi katika kibaba? Yuko nani apimaye milima kwa mizani au vilima kwa kipimo gani kingine? Yuko nani aielekezaye roho yake Bwana? Yuko nani aliyekula njama naye ya kumjulisha jambo? Yuko nani aliyepiga shauri naye la kumtambulisha kitu? Yuko nani aliyemfundisha mapito yaendayo sawasawa? Yuko nani aliyemfundisha kupambanua njia na kumjulisha utambuzi? Tazameni: mataifa mazima huwaziwa kuwa kama tone la maji katika ndoo, au kama kivumbi katika mizani! Tazameni: visiwa ni kama kichanga alichokiokota! Misitu ya Libanoni haitoshi kuwa kuni, nao nyama wake hawatoshi kuwa ng'ombe za tambiko. Mataifa yote yako mbele yake, kama si kitu, huwaziwa kuwa kama hayako kabisa na kuwa hayana maana. Mungu mtamfananisha na nani? Mtatengeneza mfano gani wa kuwa, kama yeye alivyo? Labda kinyago? Tena ni fundi aliyekiumba, kisha mfua dhahabu anakifunika chote kwa dhahabu, akakitia vinyororo vya fedha. Akosaye mali za kununua kipaji kama hicho huchagua mti usiooza, kisha hutafuta fundi aijuaye kazi hiyo, amsimamishie kinyago kisichoyumbayumba. Nanyi hamvijui? Hamvisikii? Hamkuambiwa tangu mwanzo? Hamkuitambua misingi ya nchi? Anakaa juu ya mviringo wa nchi, waikaliao wakawa kama funutu machoni pake; anazitanda mbingu kama nguo nyembamba, anaziwamba kuwa kama mahema ya kukaa. Wakuu anawatangua, wawe kama si kitu; Waamuzi wa nchi nao anawatendea, kama hawana maana. Wanapokuwa hawajapandwa, wala mbegu zao hazijamwagwa. wanapokuwa mashina yao hayajatia mizizi: mara anawapuzia, wakanyauka, kisha upepo mkali ukawachukua kama makapi. Kwa hiyo mtanifananisha na nani, niwe, kama yeye alivyo? Ndivyo, Mtakatifu anavyosema. *Yaelekezeni macho yenu juu, mtazame! Ni nani aliyeviumba hivi? Ni yeye anayevitokeza vikosi vyao hivyo, alivyovihesabu, navyo vyote pia anaviita majina. Kwa kuwa uwezo wake unazidi, nazo nguvu zake zinakaza, hakuna hata kimoja kinachokoseka. Mbona unasema, Yakobo, unanena, Isiraeli: Njia yangu imefichika, Bwana asiione, nayo maamuzi, ninayoyangojea, yamempita Mungu wangu? Hujayajua bado, hujayasikia bado? Mungu wa kale na kale ni Bwana aliyeyaumba mapeo ya nchi; hachoki, wala halegei, utambuzi wake hauchunguziki. Achokaye humpa nguvu, asiyeweza humwongezea uwezo; ijapo vijana wachoke na kulegea, ijapo wavulana nao wajikwae, lakini wamngojeao Bwana hupata nguvu mpya, waruke, kama watatumia mabawa ya kozi, hupiga mbio pasipo kulegea, hukaza mwendo pasipo kuchoka.* Ninyi visiwa, nyamazeni mbele yangu! nayo makabila ya watu na yajipatie nguvu mpya, watu na wakaribie, kisha waseme! Sote pamoja na tuje kushindana shaurini! Yuko nani aliyeamsha mtu maawioni kwa jua? Naye huyo mtu ndiye, aliyemwita mwongofu, akampatia pa kuiwekea miguu yake. Yuko nani aliyemtolea huyu mataifa, awakanyage wafalme wao, upanga wake uwaponde, wawe kama mavumbi, nao upindi wake uwatawanye kama makapi yapeperushwayo? Anapowakimbiza mwenyewe hupita salama. ijapo miguu yake isije kushika njia ya watu. Yuko nani aliyevitengeneza na kuvifanya? Yuko nani aliyeviita vizazi toka mwanzo? Ni mimi Bwana niliye wa mwanzo na wa mwisho, mimi ndiye. Visiwa vimeyaona, vikaogopa, mapeo ya nchi yakatetemeka: Wanakuja! Wamekwisha kufika karibu! Wakasaidiana kila mtu na mwenziwe, wakaambiana mtu na ndugu yake: Kaza nguvu! Mafundi wa vinyago wakawashupaza wafua dhahabu, nao wenye kuteleza dhahabu kwa nyundo ndogo wakawashupaza wapiga fuawe wakisema: Tindikali ni njema, kisha wakavipigilia misumari, visitikisike. Nawe Isiraeli uliye mtumishi wangu, nawe Yakobo, niliyekuchagua, ndiwe uzao wa mpenzi wangu Aburahamu. Nilikushika, nikakutoa kwenye mapeo ya nchi, nikakuita pembeni kwake, nikakuambia: Wewe u mtumishi wangu, nimekuchagua, sijakukataa. Usiogope! Kwani mimi niko pamoja na wewe! Usitupe macho po pote! Kwani mimi ndimi Mungu wako, ninakutia nguvu, ninakusaidia, ninakushikiza kwa mkono wangu wa kuume, nao huyanyosha yaliyopotoka. Tazama! Wote waliokutolea ukali watapatwa na soni, watamalizika, watakuwa, kama si kitu; nao waliotaka kukushinda wataangamia. Utawatafuta, usiwaone waliokupingia, waliopigana na wewe watakuwa kama si kitu chenye maana. Kwani mimi Bwana ndimi Mungu wako, ninaushupaza mkono wako wa kuume, ninakuambia: Usiogope! Mimi ninakusaidia! Usiogope, wewe Yakobo uliye kidudu, nawe Isiraeli uliye kikosi kidogo! Mimi ninakusaidia! Ndivyo, asemavyo Bwana aliyekukomboa, aliye Mtakatifu wa Isiraeli. Tazama! Nimekuweka kuwa gari jipya la kupuria lililo lenye meno makali, uiponde milima na kuibungua, vilima navyo uvifanye kuwa kama makapi. Utaipepeta, nao upepo utaichukua, nacho kimbunga kitaitawanya; nawe utampigia Bwana vigelegele, utamshangilia Mtakatifu wa Isiraeli. Wanyonge na wakiwa wako katika kutafuta maji, lakini kwa kuwa hayako, ndimi zao zimekauka kwa kiu, lakini mimi Bwana nitawaitikia, mimi Mungu wa Isiraeli sitawaacha. Nitatoa majito kwenye vilima vikavu, namo mabondeni katikati nitatoa chemchemi, nyika nitaigeuza kuwa ziwa la maji, namo jangwani maji yataonekana. Nitaotesha nyikani miangati na migunga na vihagilo na mibono; huko nyikani nitaweka mivinje na mitamba na mizambarau, kusudi wapate kuyaona na kuyatambua, wayaweke mioyoni na kujifundisha wote pamoja, ya kuwa mkono wa Bwana umeyafanya hayo, ya kuwa Mtakatifu wa Isiraeli ameyaumba. Yaleteni mabishano yenu! ndivyo, Bwana anavyosema; yafikisheni mambo yenu magumu! ndivyo, mfalme wa Yakobo anavyosema. Yafikisheni na kutusimulia yatakayokuwa! Yale ya mbele tuelezeeni maana yao, tuyaweke mioyoni, tupate kuyatambua nayo ya nyuma! Nayo yajayo tuambieni! Yatangazeni yatakayokuja nyuma, tujue, ya kuwa ninyi m miungu! Fanyizeni tu mambo yakiwa mema au mabaya, tuyastaajabu tutakapoyaona! Tazameni! Ninyi m wa bure, nazo kazi zenu huwa si kitu, anayewachagua ninyi hutapisha. Mimi nimeamsha mtu upande wa kaskazini, akaja; nimemtoa maawioni kwa jua atakayelitambikia Jina langu. Akawajia wakuu na kuwawazia kuwa mchanga, awaponde, kama mfinyanzi anavyoponda udongo. Yuko nani aliyeyaagua tangu mwanzo, tukayajua? Yuko nani aliyeyasema kale, tukayaitikia kwamba: Amesema kweli? Lakini hakuna aliyeyaagua, kweli hakuna aliyeyatangaza, wala hakuna aliyeyasikia maneno yenu. Wa kwanza mimi nimeuambia Sioni: Yatazameni! Yako! Namo Yerusalemu nimetuma mjumbe, apige mbiu njema. Lakini nilipotazama, hakuwako mtu; nako kwao hao hakuwako wa kunipa shauri, nikimwuliza, anipe majibu. Tazameni! Wote pamoja ni wa bure, nazo kazi zao huwa si kitu, vinyago vyao ni upepo mtupu pasipo maana. Mtazameni mtumishi wangu, nimshikizaye! Mtazameni mteule wangu, ambaye Roho yangu inapendezwa naye! Nitamtia Roho yangu, awatolee wamizimu habari, ya kwamba hukumu yao iko. Hatapiga kelele, wala hatalia, wala hatapaza sauti yake njiani. Utete uliokunjika hatauvunja, wala utambi unaotoka moshi bado hatauzima, aitokeze ile hukumu kuwa ya kweli. Hatazimia, wala hatashindika, mpaka yanyokayo ayashikize katika nchi, navyo visiwa vitayangoja maonyo yake. Hivi ndivyo, anavyosema Mungu Bwana aliyeziumba mbingu na kuziwamba, aliyeitanda nchi na mazao yake; watu walioko aliwapa pumzi, nazo roho aliwapa wao watembeao huku. (Anasema:) Mimi Bwana nimekuita, kwa kuwa ni mwongofu, na nikushike mkono wa kukulinda, nikuweke kuwa agano la watu na mwanga wa wamizimu, ufumbue macho ya vipofu, utoe wafungwa kifungoni, nao wakaao gizani uwatoe nyumbani, wanamolindwa. Mimi ni Bwana, hili ndilo Jina langu. Sitampa mwingine utukufu wangu, wala sitavipa vinyago mashangilio yangu. Mkitazama, yale ya kwanza yametimia, tena sasa mimi ninatangaza mapya; yanapokuwa hayajatokea bado, nawapasha ninyi habari zao. Mwimbieni Bwana wimbo mpya na kumshangilia kwenye mapeo ya nchi, ninyi mtembeao baharini nayo yote yaliyomo, ninyi visiwa nao wakaao huko! Nazo nyika na miji iliyoko ipaze sauti pamoja na vijiji, Wakedari wakaamo! Wakaao magengeni na wapige shangwe, nako vilimani kileleni na wapige makelele! Na wamtukuze Bwana! Na wayatangaze mashangilio yake visiwani! Bwana atatokea kama mwenye nguvu, kama mpiga vita atauamsha ukali, atapiga yowe na vilio, awatolee adui zake nguvu. Nimenyamaza tangu kale, nikatulia na kujizuia; lakini sasa nitalia pamoja na kufoka na kutweta kama mwanamke anayezaa. Nitachoma milima na vilima, niyanyaushe majani yao yote, nayo majito nitayageuza kuwa nchi kavu, hata mabwawa nitayakausha. Lakini vipofu nitawatembeza katika njia, wasizozijua, katika mikondo, wasiyoijua, nitawaendesha, nitaligeuza giza lililoko mbele yao kuwa mwanga, napo palipopotoka nitapanyosha. Maneno haya nitayafanya, sitayaacha. Hapo watakuwa wamerudi nyuma kwa kutiwa soni kabisa wao walioviegemea vinyago, walioviambia vinyago vilivyoyeyushwa kwa shaba: Ninyi m miungu yetu. Ninyi viziwi, sikilizeni! Ninyi vipofu, chungulieni, mpate kuona! Kipofu yuko nani, asipokuwa mtumishi wangu? Aliye kiziwi kama mjumbe wangu wa kumtuma yuko nani? Yuko nani aliye kipofu kama mpendwa? Yuko nani aliye kipofu kama mtumishi wa Bwana? Uliona mengi, lakini hukuyaangalia; alikuzibua masikio, lakini hayakusikia. Bwana kwa hivyo, alivyo mwongofu, akapendezwa kuyakuza na kuyatukuza Maonyo. Lakini sasa ukoo huu ni ukoo wa watu walionyang'anywa na kupokonywa mali zao, wote pia wamenaswa miinani, wakafichwa nyumbani mwa kufungia watu, wakatekwa, tena hakuna aliyewaopoa, wakapokonywa mali zao, tena hakuna aliyesema: Rudisha! Kwenu yuko nani atakayeyasikia hayo? Yuko nani atakayeyaangalia atakapoyasikia huko nyuma? Ni nani aliyemtoa Yakobo, apokonywe mali zake? Ni nani aliyemtia Isiraeli mikononi mwa wanyang'anyi? Si mimi Bwana, waliyemkosea, walipokataa kuzishika njia zangu na kuyasikia Maonyo yangu? Ndipo, alipowamiminia makali yake yaliyo yenye moto na makorofi ya vita, yakamzunguka na kumchoma lakini hakujua maana, yakamwunguza, lakini hayakumfikia moyoni. Hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliyekuumba, Yakobo, aliyekutengeneza, Isiraeli: Sasa usiogope! Kwani nimekukomboa, nimekuita kwa jina lako, ndiwe wangu! Utakapopita majini, mimi niko pamoja na wewe; utakapopita katika majito, hayatakutosa; utakapopita motoni hutachomwa, wala ndimi za moto hazitakuunguza. Kwani mimi Bwana Mungu wako, Mtakatifu wa Isiraeli, mimi mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa makombozi yako, nikatoa Nubi na Seba mahali pako. Kwa kuwa uliwaziwa machoni pangu kuwa mali, umepata utukufu, nikakupenda. Kwa hiyo nimetoa watu, nikukomboe, hata makabila mazima, niikomboe roho yako. Usiogope! Kwani mimi niko pamoja na wewe; walio uzao wako nitawaleta na kuwatoa maawioni kwa jua, nitawakusanya na kuwatoa nako machweoni kwa jua. Nitauambia upepo wa kaskazini: Watoe! nao upepo wa kusini: Usiwazuie! Walete wanangu wa kiume na kuwatoa mbali nao wanangu wa kike na kuwatoa mapeoni kwa nchi, wao wote waitwao kwa Jina langu! Ndio, niliowaumba, nijipatie utukufu, ndio, niliowatengeneza na kuwafanya. Watokezeni watu walio vipofu! Tena macho wanayo. Nao walio viziwi! Tena masikio wanayo. Wamizimu wote na wakusanyike pamoja, makabila ya watu na yakutane; kwao yuko nani aliyetangaza kama hayo? Yuko nani aliyetuambia yale ya mbele? Na watoe mashahidi, wapate kushinda shaurini, watu wayasikie, kisha waseme: Ni kweli! Ninyi m mashahidi wangu! ndivyo, asemavyo Bwana, u mtumishi wangu, niliyekuchagua kwamba: Mjue, mpate kunitegemea, tena mtambue, ya kuwa mimi ndiye! Mbele yangu hakufanyika Mungu, hata nyuma yangu hatakuwa. Mimi ndimi Bwana, pasipo mimi hakuna mwokozi. Mimi nimeyatangaza, nikatengeneza wokovu, nikaujulisha, mkingali hamna mungu mgeni kwenu; nanyi m mashahidi wangu, nami ndimi Mungu! ndivyo, asemavyo Bwana. Tena tangu leo nitakuwa yeye niliyekuwa, hakuna aopoaye mkononi mwangu; nikitaka kufanya kitu, yuko nani atakayekizuia? Hivi ndivyo, anavyosema Bwana, mkombozi wenu, aliye Mtakatifu wa Isiraeli: Kwa ajili yenu nilituma watu kwenda Babeli, niwakimbize wote pia, washuke mtoni, nao Wakasidi na wakimbie katika vyombo vyao, walivyovipigia shangwe. Mimi Bwana ndimi Mtakatifu wenu, mimi niliyemwumba Isiraeli ndimi mfalme wenu. Hivi ndivyo, anavyosema Bwana awekaye njia baharini, hata mapito katika maji yenye nguvu, atokezaye magari na farasi, vikosi na wakuu pamoja: Mara wataanguka, wasiinuke tena, watazimia, kama utambi unavyozimika. Msiyakumbuke yaliyoko mbele, wala msiyatambue yaliyopita kale! Tazameni! Ninafanya mapya, nayo yameanza kuchipuka! Nanyi hamjayaona bado? Hata nyikani ninatoa njia, nako jangwani majito. Nyama wa porini watanitukuza, mbwa wa mwitu na mbuni, kwa kuwa nimetoa maji nyikani na majito jangwani, niwanyweshe wao, niliowachagua, wawe ukoo wangu. Hao watu, niliojitengenezea, watayasimulia na kushangilia. Nawe Yakobo, hukuniita mimi, nawe Isiraeli, hukujichokesha kwa ajili yangu. Hukuniletea wana kondoo wako kuwa wa kunitambikia, wala hukuniheshimu na kunitolea vipaji vya tambiko. Nami sikukusumbua, unipatie matunzo, wala sikukuchokesha na kutaka uvumba kwako. Hukuninunulia vipande vya kichiri na kutoa fedha zako, wala hukuninywesha mafuta ya ng'ombe zako za tambiko. Ila ulinisumbua kwa makosa yako, ukanichokesha kwa manza zako, ulizozikora. Mimi ninayafuta mapotovu yako kwa ajili yangu mimi, nayo makosa yako sitayakumbuka tena. Nikumbushe, tubishane! Nawe yaseme yako, upate kushinda humu shaurini! Baba yako wa kwanza alikosa naye, nao wasemaji wako walinitengua. Ndipo, nilipowatia mwiko wakuu wa Patakatifu, nikamtoa Yakobo kuwa wa kuapizwa naye Isiraeli kuwa wa kufyozwa. *Sasa sikia mtumishi wangu Yakobo! Nawe Isiraeli, niliyemchagua! Hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliyekuumba, aliyekutengeneza tumboni mwa mama, anayekusaidia: Usiogope, mtumishi wangu Yakobo, nawe Isiraeli uongokaye, niliyemchagua! Kwani nitamwaga maji panapo kiu, nitokeze mito pakavu, nitaimwaga Roho yangu kwao walio uzao wako, nayo mbaraka yangu kwao walio miche yako. Watakuwa kama majani kwenye maji au kama mifuu kwenye mito yenye maji. Huyu atasema: Mimi ni wake Bwana, naye mwenziwe atajiita kwa jina la Yakobo, naye mwingine ataandika mikononi mwake: Wa Bwana, mwingine atajivunia jina la Isiraeli, Hivi ndivyo, anavyosema Bwana, mfalme wa Isiraeli, aliye mkombozi wake, yeye Bwana Mwenye vikosi: Mimi ni wa mwanzo na wa mwisho, pasipo mimi hakuna Mungu.* Yuko nani anayefanana na mimi? Na apaze sauti, ayatangaze! Tena anieleze, kama ni kwa sababu gani, nikiweka ukoo wa watu kuwa wa kale na kale. Hata yajayo nayo yatakayokuja na wayatangazie watu! Msistuke, wala msitetemeke! Kumbe sikukuambia hayo toka kale na kuyatangaza? Ninyi m mashahidi wangu: Yuko Mungu pasipo mimi? Hakuna mwamba mwingine, nisioujua. Watengenezao vinyago wote si kitu, navyo viumbe vyao vya kupendeza havifai, wanaovishuhudia wenyewe hawaoni, wala hawatambui kazi, ambazo vilizifanya, kusudi wapatwe na soni. Ni nani aliyetengeneza mungu na kuyeyusha kinyago kisichofaa kitu? Tazameni! Wote walio upande wao hupatwa na soni, nao mafundi na watu tu. Na wakusanyike wote pamoja na kusimama hapa, wote pamoja watastuka na kupatwa na soni. Mhunzi huvishika vyombo vyake, hutumia moto wa makaa akivitengeneza vinyago kwa vyundo; hivyo anavimaliza kwa mkono wake wenye nguvu; lakini asipokula, nguvu hupotea, napo asipokunywa hulegea. Fundi wa kuchonga miti huipima kwa kamba na kuiandika kwa kalamu; kisha hutumia visu na kupimapima tena penye kuviringana. Hivyo anatengeneza kinyago, kifanane na mtu mwenye utukufu wa kimtu, kikae nyumbani. Huagiza watu, wamkatie miangati, huchukua hata mipingo na mivule, hujichagulia miti ya mwituni iliyo migumu, hupanda nayo mise, mvua iikuze. Watu huitumia ya kuchoma moto, huchukua vibanzi vyao vya kuotea, vingine huvitumia jikoni vya kuchomea mikate, tena kipande hukitengeneza kuwa mungu wa kuuangukia; alipokwisha kufanya kinyago, hukitambikia. Hivyo hutumia kipande cha mti cha kuchoma moto, apate kuota, kipande cha kupikia nyama, ale nazo zilizochomwa, ashibe, apate hata jasho, aseme: A, nimepata jasho, nimeona moto! Kipande kinachosalia hukitengeneza kinyago kuwa mungu, hukitambikia na kukiangukia na kukilalamikia kwamba: Niponye! Kwani mungu wangu ndiwe wewe! Lakini hawa hawavijui wala hawavitambui, kwani macho yao yamegandamana, yasione, mioyo yao isielewe maana. Hakuna ayawazaye moyoni, wala hakuna ayajuaye na kuyatambua kwamba: Kipande chake nimekichoma moto, kipande nimetumia makaa yake, yachome mkate, kipande nimechoma cha kuchomea nyama, nikala. Tena sao lake nilitengeneze kuwa chukizo, nitambikie kilicho kipande cha mti? Ni hivyo: Achungaye majivu moyo wake umedanganyika, ukampoteza, asiiponye roho yake, wala asiseme: Siyo yenye uwongo yaliyomo mkononi mwangu? Haya yakumbukeni, Yakobo na Isiraeli! Kwani wewe ndiwe mtumishi wangu; nimekutengeneza wewe kuwa mtumishi wangu, wewe Isiraeli hutasahauliwa kwangu. Nimeyatowesha mapotovu yako kama wingu, nayo makosa yako kama kungugu. Rudi kwangu! Kwani nimekukomboa. Shangilieni, mbingu, ya kuwa Bwana ameyatimiza! Pigeni kelele, vilindi vya kuzimuni! Pigeni shangwe na kupaza sauti, milima na misitu na miti yote iliyomo! Kwani Bwana amemwokoa Yakobo, nako kwake Isiraeli anautokeza utukufu wake. Hivi ndivyo, anavyosema Bwana, mkombozi wako, aliyekutengeneza tumboni mwa mama: Mimi Bwana niliyafanya yote. Mimi nilipoziwamba mbingu peke yangu, nikazitanda hata nchi, yuko nani aliyekuwa kwangu? Ndege, wapuzi wanazoziona, nazibezesha, nao waaguaji nawalevya, nao walio werevu wa kweli nawarudisha nyuma, ujuzi wao naugeuza kuwa ujinga. Neno la mtumishi wake hulisimamisha, nayo mashauri ya wajumbe wake huyatimiza. Ni yeye auambiaye Yerusalemu: Na ukaliwe! Nayo miji ya Yuda anaiambia: Jengweni! Nami nitayasimamisha mabomoko yao! Kilindi cha maji anakiambia: Kauka! mimi nitaipwelesha mito yako. Yeye ndiye anayemwambia Kiro: Huyu ndiye mchungaji wangu atakayeyatimiza mapenzi yangu yote. Hivyo Yerusalemu utajengwa, nalo Jumba takatifu litawekewa misingi. Hivi ndivyo, Bwana anavyomwambia Kiro, aliyempaka mafuta: Nimemshika mkono wake wa kuume, nikanyage mbele yake mataifa mazima, nikafungua mishipi viunoni kwa wafalme, nikafungua mbele yake milango na malango, yasifungike tena. Mimi nitakwenda mbele yako, nipalinganye pasipopitika, nivunje milango ya shaba, nikate makomeo ya chuma. Nitakupa malimbiko yaliyomo gizani nazo tunu zilizofichwa, kusudi upate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana, Mungu wa Isiraeli ndiye aliyekuita kwa jina lako. Ni kwa ajili ya mtumishi wangu Yakobo na kwa ajili ya mteule wangu Isiraeli, nikikuita kwa jina lako na kukupa jina la macheo, nawe ulikuwa hukunijua. Mimi ni Bwana, hakuna mwingine tena; pasipo mimi hakuna Mungu; nimekuvika, nawe ulikuwa hukunijua. Kwani walioko maawioni nao walioko machweoni kwa jua ninawataka wote, wajue, ya kuwa hakuna aliye Mungu, isipokuwa mimi, mimi ni Bwana, hakuna mwingine tena. Natengeneza mwanga, naumba giza nayo, nafanya utengemano, naumba ubaya nao, mimi Bwana ndiye ayafanyaye hayo yote. Ninyi mbingu, nyesheni huko juu, nanyi mawingu umimineni wongofu, nchi ifunguliwe, ijae wokovu, ioteshe wongofu nao; mimi Bwana ndiye aliyeiumba. Yatampata ambishiaye mfinyanzi wake, naye ni kigae tu kwenye vigae wenziwe vya udongo! Je? Udongo unaweza kumwambia mfinyanzi: Unafanya nini? Au kiko kiumbe chako kiwezacho kukuambia: Hana mikono? Yatampata amwambiaye baba yake: Watoto unawazalia nini? au amwambiaye mama yake: Mimba unazipatia nini? Hivi ndivyo, anavyosema Bwana, Mtakatifu wa Isiraeli, yeye aliyemtengeneza asema: Niulizeni yatakayokuja! Niagizieni nayo mambo ya watoto wangu! Kwani ndio kazi za mikono yangu. Mimi nilifanya nchi, nikawaumba watu waikaao; mikono yangu mimi iliziwamba mbingu, navyo vikosi vyao vyote niliviagiza, vitokee. Mimi nimemwamsha naye yeye (Kiro) kwa hivyo, nilivyo mwongofu, nazo njia zake zote na nizinyoshe. Yeye ndiye atakayeujenga mji wangu, nao watu wangu waliotekwa atawafungua, wajiendee; lakini havitakuwa kwa makombozi wala kwa fedha za kupenyezewa. Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Wamisri na mali zao, walizozisumbukia, nao Wanubi na mapato yao, waliyoyachuuzia, nao Waseba, wale watu warefu, watakufikia, wawe wako; wakikuangukia na kukulalamikia, watakwenda nyuma yako wakiwa wamejifunga mapingu, kwani kwako yuko Mungu, hakuna mwingine tena awaye yote aliye Mungu. Wewe ndiwe Mungu kweli, ijapo uwe mwenye mafumbo, u Mungu wa Isiraeli, u mwokozi. Wao wote pamoja watakuwa wameona soni kwa kutwezwa, mafundi wa vinyago watakuwa wamejiendea kwa kutwezwa. Isiraeli atakuwa ameokolewa na Bwana, atapata wokovu wa kale na kale, hamtaona soni, wala hamtatwezeka siku za kale na kale zitakazokuwa zote. Kwani hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliyeziumba mbingu, yeye Mungu, aliyeifanya nchi na kuitengeneza vema, yeye aliyeishikiza, kwa kuwa hakuiumba, iwe tupu, yeye aliyeitengeneza, watu waikae, yeye anasema: Mimi ndimi Bwana, hakuna mwingine tena. Sikusema fichoni mahali penye giza ya nchi, wala sikuwaambia walio uzao wa Yakobo: Nitafuteni bure! Mimi Bwana husema yenye wongofu, hutangaza yanyokayo! Njoni, kusanyikeni, mfike karibu, ninyi masao ya wamizimu mliopona! Hawajui kitu wajitwikao vinyago vya miti kulalamikia mungu usioweza kuokoa. Semeni, leteni mashahidi! Na wapige shauri pamoja! Yuko nani aliyeambia watu haya, wakiyasikia huko kale? Yuko nani aliyeyatangaza tangu mwanzo? Si mimi Bwana? Hakuna tena aliye Mungu, isipokuwa mimi. Mungu aliye mwongofu na mwokozi hayuko pasipo mimi. Nigeukieni, mwokoke, ninyi mapeo yote ya nchi! Kwani mimi ndimi Mungu, hakuna mwingine tena. Nimeapa na kujitaja mwenyewe, neno lenye wongofu likatoka kinywani mwangu, nalo halitarudi bure, hilo la kwamba: Mimi wote watanipigia magoti, ndimi zao zote zikisema kwa kuapa: Kwake Bwana peke yake ndiko, nilikopata wongofu na nguvu. Sharti waje kwake na kuona soni wote waliomkasirikia. Kwake Bwana watapata wongofu, kisha watamshangilia wote walio wa uzao wake Isiraeli. Beli ameanguka, Nebo naye yuko chini, vinyago vyao viko migongoni kwa punda na ng'ombe; vilivyotembezwa nanyi vimefungwa, ikawa mizigo ya kuchokesha nyama wanaoichukua. Wako chini pamoja, kama walivyoanguka pamoja, hawakuweza kuviokoa vinyago, visichukuliwe, wao wenyewe wamekwenda kufungwa kwa kuwa mateka. Nisikilizeni, ninyi mlio wa mlango wa Yakobo! Ninyi wote mlio masao ya mlango wa Isiraeli! Ninyi ndio, niliojitwika tangu hapo, mlipokuwa tumboni mwa mama zenu, ninyi ndio, niliojichukuza tangu hapo, mlipozaliwa. Hata mtakapokuwa wazee, mimi ndimi niliyekuwa; hata mtakapotoka mvi, mimi nitawachukua. Mimi nitayafanya nikijitwika mimi, mimi nitawachukua na kuwaokoa. Yuko nani, ambaye mtanifananisha naye, tuwe sawa? Yuko nani, ambaye mtanilinganisha naye, tufanane? Watu humwaga dhahabu toka mifukoni, hupima fedha kwa mizani, humlipa fundi, naye hufanya mungu, wauangukie na kuutambikia. Kisha huuchukua mabegani, huutembeza, kisha huuweka mahali pake; hapo unasimama pasipo kuondoka mahali pake. Wanapoulilia, hauwaitikii; hakuna, umwokoaye katika shida yake. Haya yakumbukeni, mjishupaze! Yawekeni mioyoni, ninyi wapotovu! Yakumbukeni yale ya mwanzo yaliyokuwapo tangu kale! Kwani mimi ndimi Mungu, hakuna mwingine tena, kweli, hakuna Mungu aliye kama mimi. Tangu mwanzo nayatangaza yatakayokuwa mwisho, toka kale nayasema yasiyofanyika bado. Kila nisemapo, shauri langu litatimia, yote yanipendezayo mimi huyafanya. Ninaita kipanga maawioni kwa jua, katika nchi ya mbali ndiko, ninakotoa mtu atakayelifanya shauri langu. Kama nilivyosema, ndivyo, nitakavyoyatimiza; kama nilivyoyalinganya, ndivyo, nitakavyoyafanya. Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu, ninyi mliojitenga na kuyaacha mbali yaliyoongoka! Yale yaongokayo nimeyafikisha karibu, hayako mbali tena, wokovu wangu haukawilii. Sioni ndimo, nitakamotokeza wokovu, kwao Waisiraeli ndiko, nitakakotokeza utukufu wangu. Shuka, ukae mavumbini, binti Babeli uliye mwanamwali! Kaa chini! Hakuna kiti kitukufu, mwana wa Wakasidi! Hutaitwa tena mwanana mwenye mwili mzuri. Chukua jiwe la kusagia, jike na dume, usage unga mwenyewe ukiisha kuuvua ukaya wako! Pandisha nguo, mapaja yaoneke, ukipita mito! Uchi wako na ufunuliwe, nayo yakutiayo soni yaoneke! Nitakulipisha hivyo, hakuna nitakayemhurumia. Mkombozi wetu ni Bwana Mwenye vikosi, Jina lake ni Mtakatifu wa Isiraeli. Nyamaza kimya, uende zako gizani, mwana wa kike wa Wakasidi! Kwani hawatakuita tena bibi mwenye nchi za kifalme. Nilipowakasirikia walio ukoo wangu, ndipo, nilipowachafua walio fungu langu, nikawatia mikononi mwako, lakini wewe hukuwahurumia, ukawatwika nao wazee mizigo yako iliyowalemea sana. Ukasema kwamba: Kale na kale nitakuwa mfalme! Kwa hiyo hukuyawaza hayo moyoni, wala hukukumbuka, ya kuwa yako na mwisho. Sasa yasikie haya, wewe mcheshi uliyekaa salama, uliyesema moyoni mwako: Ni mimi, hakuna mwingine tena! Sitakaa ujane, wala sitakujua kuwa pasipo watoto. Tena yatakujia siku moja na kukugundua hayo mambo mawili: kuwa pasipo watoto na kukaa ujane; haya yatakujia yote pamoja, ijapo mazindiko yako yawe mengi, ijapo kugangua kwako kuwe kwenye nguvu sana. Ulijiegemeza kwa ubaya wako ukisema: Hakuna anayeniona. Werevu wako na ujuzi wako ukakuponza, ukasema moyoni mwako: Ni mimi, hakuna mwingine tena! Basi, mabaya yatakujia, usiyojua kuyalogoa; teso litakuangukia, usiloweza kujizindikia. Mara angamizo litakujia, usilolijua. Jisimamie hapo, unapogangua, panapo mazindiko yako mengi, ambayo ulijisumbua nayo tangu ujana wako; labda utaweza kujipatia mafaa, labda utastusha watu. Umechokeshwa na mashauri yako mengi; sasa na watokee, wakuokoe, wao waaguliao ya mbinguni nao wachunguzao nyota, wao waliolinganya kila mwandamo wa mwezi upande, yatakakotokea mabaya yatakayokujia. Watazameni! Wako kama makapi yaliyounguzwa na moto, hawawezi kujiokoa wenyewe katika moto uwashikao, hakuna makaa ya kuyaotea, wala hakuna jiko lenye moto la kukaa hapohapo. Ndivyo, walivyokufanyia nao wachuuzi wako, uliowasumbukia tangu ujana wako, wametawanyika, kila mmoja upande wake, hakuna akuokoaye. Yasikieni haya, ninyi wa mlango wa Yakobo! Mnajiita kwa jina la Isiraeli, mlitoka viunoni mwa Yuda, mnaapa na kulitaja Jina la Bwana, naye Mungu wa Isiraeli mnamtukuza; lakini si kwa kweli wala kwa wongofu. Wanajiita kwa jina la mji mtakatifu, wanajishikiza kwake Mungu wa Isiraeli, Bwana Mwenye vikosi na Jina lake. Yale ya mbele, niliyoyatangaza hapo kale, yalitoka kinywani mwangu, nikawaambia, myasikie; maana nitakapoyafanya, yatatimia. Kwani nimekujua, ya kuwa u mgumu, ya kuwa ukosi wako ni mshipa wa chuma, ya kuwa kipaji cha uso wako ni shaba. Nikakutangazia hapo kale, nikakuambia uyasikie, yalipokuwa hayajatimia bado, usiseme: Kinyago changu kimeyafanya! wala: Kinyago changu cha mti uliochongwa au cha shaba iliyoyeyushwa kimeyaagiza! Umeyasikia, basi, yatazame hayo yote! Mbona ninyi hamyaungami? Tangu sasa ninakuambia mapya, uyasikie, ni mambo yaliyofichwa, usiyoyajua bado. Yameumbwa sasa, si kale; mpaka leo hukuyasikia bado, usiseme: Hayo nimekwisha kuyajua. Kweli hukuyasikia, wala hukuyajua, wala masikio yako hayajazibuka, kwani nimekujua, ya kuwa u mdanganyifu, ukaitwa mpotovu tangu kuzaliwa kwako. Ni kwa ajili ya Jina langu, nikayakawilisha makali yangu kwa kwamba: Na wanishangilie, nikajizuia, nisikujie, nikakung'oa. Tazama! Nimekung'aza na kukuyeyusha, lakini sikukuona kuwa fedha; nikakujaribu na kukutia motoni mwenye mateso. Kwa ajili yangu mimi nimeyafanya, Jina langu lisitiwe uchafu; maana utukufu wangu sitampa mwingine. Nisikilize, Yakobo, nawe Isiraeli, niliyekuita! Mimi ndiye! Mimi ni wa kwanza, tena mimi ni wa mwisho. Mkono wangu ndio uliozishikiza nchi, mkono wangu wa kuume ndio ulioziwamba mbingu; ninapoyaita yawayo yote, ndipo, yanapotokea. Kusanyikeni ninyi nyote, msikie! Kwao yuko nani aliyeyatangaza haya ya kwamba: yeye, Bwana ampendaye, ataufanyia Babeli yampendezayo, nao mkono wake utawatokea Wakasidi? Mimi ndimi niliyeyasema! Kisha nikamwita, nikamleta, naye na aitimize njia yake. Nifikieni karibu, myasikie haya! Tangu mwanzo sijasema mafichoni, tangu hapo yalipokuwapo mimi nipo! Na sasa Bwana Mungu amenituma na kunipa roho yake. Ndivyo, anavyosema Bwana aliyekukomboa, aliye Mtakatifu wa Isiraeli: Mimi Bwana ndimi Mungu wako; ninakufundisha yafaayo, ninakuongoza katika njia, utakayoishika. Kama ungaliyaangalia maagizo yangu, utengemano wako ungalikuwa kama mto, nao wongofu wako ungalikuwa kama mawimbi ya bahari. Wao wa uzao wako wangalikuwa wengi kama mchanga, nao waliotoka mwako wangalikuwa wengi kama vijiwe vya chembe yake. Majina yao hayatang'olewa hayataangamia mbele yangu. Tokeni Babeli! Wakimbieni Wakasidi! Yatangazeni na kupiga vigelegele, yasikilike mpaka mapeoni kwa nchi, mkiyatokeza kwamba: Bwana amemkomboa mtumishi wake Yakobo! Hawakupata kiu, alipowapitisha majangwani, akawatolea maji miambani; alipopasua miamba, maji yakabubujika. Lakini hakuna utengemano kwo wasiomcha Mungu; ndivyo, Bwana anavyosema. Nisikieni, ninyi visiwa, nanyi makabila ya watu mlioko mbali, tegeni masikio! Bwana aliniita hapo nilipozaliwa, akalikuza jina langu tangu hapo, nilipotoka tumboni mwa mama. Akakitumikisha kinywa changu kama upanga mkali, akanificha kivulini mwa mkono wake, akanitumia kuwa mshale umetukao, akanificha katika podo lake. Akaniambia: Ndiwe mtumishi wangu, wewe Isiraeli ndiwe, ambaye nitajitukuzia. Nami nalisema: Nimejichokesha bure, nikizimaliza nguvu zangu na kusumbukia mambo yasiyo na maana, yasiyo kitu. Lakini yanipasayo yako na Bwana, mapato yangu yako na Mungu wangu. Sasa nimeambiwa neno na Bwana aliyenitengeneza tumboni mwa mama kuwa mtumishi wake wa kumrudisha Yakobo kwake, Waisiraeli wapate kukusanyika kwake; kwani nimetukuka machoni pa Bwana, Mungu wangu akawa nguvu zangu. Amesema hivi: Haitoshi, ukiwa mtumishi wangu wa kuiinua milango ya Yakobo na wa kuwarudisha Waisiraeli waliookoka, nimekuweka tena kuwa mwanga wa wamizimu, wokovu wangu ufike mapeoni kwa nchi. Hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliyemkomboa Isiraeli, ndivyo, Mtakatifu wake anavyomwambia yeye, watu wanayembeza na kumchukia mioyoni mwao, aliye mtumishi wao wanaoitawala nchi: Wafalme watayaona, nao wakuu watainuka, wakuangukie, kwa kuwa Bwana ni mtegemevu, kwa kuwa ndiye Mtakatifu wa Isiraeli aliyekuchagua. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nimekuitikia, siku zilipokuwa za kupendezwa, nikakusaidia siku ya wokovu, nikulinde, nikuweke kuwa agano lao walio ukoo wangu, uichipuze nchi, uwagawie wenyewe mafungu yao yaliyokufa, uwaambie wafungwa: Tokeni! nao waliomo gizani: Kesheni! Watalisha njiani, napo vilimani po pote palipokuwa pakavu wataona malisho yao. Hawataona tena njaa wala kiu, hawatapigwa na upepo wenye joto wala na jua, kwani awahurumiaye atawaongoza, awapeleke kwenye visima vya maji. Nayo milima yangu yote nitaiweka kuwa njia, nazo barabara zangu zitapitia juu. Na mwaone watakaotoka mbali: wengine watatoka upande wa kaskazini, wengine upande wa baharini, wengine nchi ya Sinimu. Shangilieni mbingu! Nawe nchi, piga vigelegele! Nayo milima na ipige shangwe! Kwani Bwana amewatuliza walio ukoo wake, akawahurumia wanyonge walio wake. Sioni ulisema: Bwana ameniacha; Bwana wangu amenisahau. Je? Mwanamke humsahau mtoto wake mnyonyaji, asimhurumie mwana, aliyemzaa? Ijapo amsahau, mimi sitakusahau kamwe. Tazama! Nimekuchora maganjani mwangu, kuta zako haziondoki machoni pangu. Wanao wa kiume wanakuja na kupiga mbio, lakini wao waliokuvunja na kukubomoa watakutoka. Yainue macho yako na kuyazungusha, uone! Hawa wote wamekusanyika, wafike kwako! Ndivyo, asemavyo Bwana: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, hawa wote utawavaa kama mapambo, utawatumia kuwa kama ukanda wa mchumba mke. Kwani mahame na mapori yako na mashamba yako yaliyokufa sasa hayatawaeneza watakaokuja, wakae, nao waliokumeza watakuwa wamekwenda mbali. Itakuwa, wanao waliozaliwa katika ukiwa wako wasemeane masikioni mwako: Pangu ni padogo, sogeza, ndugu yangu, nipate kukaa! Nawe utasema moyoni mwako: Ni nani aliyenizalia hawa? Mimi nilikuwa sina watoto, maana nilikuwa mgumba, nilikuwa nimetekwa, nikapelekwa mbali. Basi, ni nani aliyewakuza hawa, nilipokuwa nimesazwa peke yangu? Wanatoka wapi hawa? Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Tazama! Nitawapungia wamizimu kwa mkono wangu, nitawatwekea makabila ya watu bendera yangu; ndipo, watakapowaleta wanao na kuwabeba vifuani, nao watoto wako wa kike watawachukua mabegani. Wafalme watakuwa walezi wako, nao wake wa kifalme watakuwa wanyonyeshaji wako, watakuangukia kifudifudi, walambe mavumbi miguuni pako; ndipo, utakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, ya kuwa hawapatwi na soni waningojeao. Je? Mwenye nguvu atachukuliwa mateka yake? Au kole zake mwongofu zitakombolewa? Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kweli nazo kole za mwenye nguvu zitachukuliwa, nayo mateka ya mkorofi yatapona; maana wao waliokugombeza nitawagombeza mimi, nao wanao nitawaokoa mimi. Waliokutesa nitawalisha nyama zao, wanywe damu zao kama ni pombe, mpaka walewe; ndipo, wote wenye miili ya kimtu watakapojua, ya kuwa mimi ndimi Bwana, mwokozi wako, ni mkombozi wako akutawalaye, Yakobo. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kiko wapi cheti cha kuachana, nilichompa mama yenu nilipomtuma kujiendea? Au yuko nani aliyenidai, nikawauza ninyi kwake? Tazameni: Mmeuzwa kwa ajili ya manza zenu, mlizozikora; tena ni kwa ajili ya mapotovu yenu, mama yenu akitumwa kujiendea. Ilikuwaje, nisione mtu nilipofika? Au nilipoita, asijibu mtu? Je, Mokono wangu ulikuwa mfupi, usiweze kukomboa? Au je? Sinazo nguvu za kuponya? Tazameni! Kwa nguvu za makemeo yangu naikausha bahari, nayo mito naigeuza kuwa jangwa, samaki wao wanuke kwa kukosa maji wanapokufa kwa kiu. Mbingu nazivika weusi, ninapozifunika kama kwa gunia. Bwana Mungu amenipa ulimi uliojifunza, mpaka ukijua kuegemeza mchovu kwa kusema naye, huniamsha kunapokucha, huliamsha sikio langu, lisikilize, kama wenye kujifunza wanavyosikiliza. Bwana Mungu amenizibua sikio, nami sikukataaa, wala sikurudi nyuma. Mgongo wangu nimeuelekezea wao walionipiga, nayo mashavu yangu wao walioning'oa ndevu, uso wangu sikuufichia wao walionitweza, ndio wao walionitemea mate. Bwana Mungu akanisaidia, kwa hiyo sikutwezeka, kwa hiyo nikaushupaza uso wangu kuwa kama jiwe la moto, nikajua, ya kuwa sitaiva uso. Yuko karibu atakayenishindisha; yuko nani atakayenigombeza? Na tutokee kusimama pamoja! Yuko nani atakayenipeleka shaurini? Na aje, twende! Na mwone, ya kuwa Bwana Mungu ananisaidia! Yuko nani atakayenishinda? Na mwone, ya kuwa hawa wote watachakaa kama nguo, ikiliwa na nondo! Yuko nani kwenu anayemwogopa Bwana? Yuko nani kwenu anayeisikiliza sauti ya mtumishi wake? Akienda gizani pasipo kumulikiwa na aliegemee Jina la Bwana! Na ajikongojee Mungu wake! Sasa ninyi nyote mnaowasha moto, mwikoleze mishale ya moto, nendeni kuunguzwa na moto wenu, mishale, mliyoiwasha, iwachome moto! Hayo yatatokea mkononi mwangu, yawajie, mlazwe mahali panapoumiza. Nisikilizeni, ninyi mnaofuata yaongokayo, ninyi mnaomtafuta Bwana! Utazameni mwamba, ambao mlichongwa mumo humo! Litazameni shimo la kisima, ambalo mlichimbuliwa mumo humo! Mtazameni baba yenu Aburahamu na mzazi wenu Sara! Nilimwita yeye mmoja tu, nikambariki, nikampa kuwa wengi. Kwani Bwana ameutuliza Sioni, ameyatuliza mabomoko yake yote, kwa kuwa atayageuza mapori yake kuwa mashamba, nazo nyika zake kuwa kama bustani ya Bwana. Ndipo, kutakapooneka mle kufurahi na kuchangamka, kushukuru na kuimba kwa sauti kuu. Niangalieni, ninyi mlio ukoo wangu, ninyi mlio watu wangu nisikilizeni! Kwani maonyo yatatoka kwangu, nayo yanyokayo machoni pangu nitayaweka kuwa mwanga wa makabila ya watu. Bado kidogo nitakuja kushinda na kuutokeza wokovu wangu; ndipo, mikono yangu itakapoyapatiliza makabila ya watu. Mimi ndimi, visiwa vitakayemngojea na kuuchungulia mkono wangu. Yaelekezeni macho yenu mbinguni! Kisha zitazameni nchi zilizoko chini! Kwani mbingu zitatoweka kama moshi, nazo nchi zitachakaa kama nguo, nao wazikaliao mara watakufa vivyo hivyo. Lakini wokovu wangu utakuwa wa kale na kale, nao wongofu wangu hautaangamika. Nisikilizeni, ninyi mjuao yaongokayo, mlio watu wayashikao Maonyo yangu mioyoni mwenu, msiogope kutwezwa na watu, wala msiyastukie matusi yao! Yako yatakayowala, kama nondo wanavyokula nguo, au kama mende wanavyokula pamba, lakini wongofu wangu utakuwa wa kale na kale, nao wokovu wangu utakalia vizazi na vizazi. Amka! Amka, uone nguvu, wewe mkono wa Bwana! Amka kama siku za kale kwenye vizazi vya zamani! Si wewe uliomkatakata Rahabu (Mkuu wa maneno wa Misri) na kumchoma yule joka kubwa? Si wewe ulioikausha bahari yenye vilindi vya maji mengi na kutoa njia mlemle vilindini mwa bahari, wapitemo waliokombolewa? Waliookolewa na Bwana watarudi, waje Sioni na kupiga shangwe; vichwani pao itakuwa furaha ya kale na kale, machangamko na furaha zitawafikia, lakini machungu yatakimbia, wasipige kite tena. Mimi ndimi ninayewatuliza mioyo yenu. Wewe ndiwe nani ukiogopa watu wafao na wana wa watu watowekao kama majani? Umemsahau Bwana aliyekufanya, aliyezitanda mbingu, aliyezishikiza nchi, ukatetemeka siku zote pasipo kukoma kwa ajili ya makali yake anayekusonga, kwa kuwa alitaka kukuangamiza; na sasa makali yake aliyekusonga yako wapi? Aliyepindika kwa kufungwa atafunguliwa upesi, hatakufa, atupwe shimoni, wala hatakosa chakula chake. Kwani mimi na Bwana Mungu wako, achafuaye bahari, mawimbi yake yaumuke; Bwana Mwenye vikosi ni Jina langu. Nami nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako, nikakuficha kivulini mwa mkono wangu, nipate kuzitokeza mbingu mpya na kuishikiza nchi tena, na kuuambia Sioni: Ukoo wangu ndiwe wewe. Amka! Amka! Inuka, Yerusalemu! Umekunywa mkononi mwa Bwana kikombe chenye makali yake, hicho kikombe kilichojaa kileo cha kupepesusha umekinywa na kukimaliza. Katika watoto wote, aliowazaa, hakuwako, aliyemwongoza, wala katika watoto wote, aliowakuza, hakuwako, aliyemshika mkono. Mambo yaliyokupata ni haya mawili, -lakini yuko nani atakayekupongeza?- kuvunjwa na kubomolewa, tena kuuawa kwa njaa na kwa panga, lakini nitawezaje kukutuliza moyo? Wanao wa kiume walikuwa wamezimia, wakalala pembeni kwenye njia zote za mji, wakawa kama paa waliokamatwa na wavu, kwa kuwa walileweshwa na makali yake Bwana, na makemeo yake Mungu wako. Kwa hiyo yasikilize haya, wewe uliyenyongeka kwa kulewa, lakini sio kwa mvinyo! Ndivyo, anavyosema Bwana aliye Bwana na Mungu wako, awapiganiaye walio ukoo wake: Tazama! Nimekichukua mkononi mwako kile kikombe chenye kileo cha kupepesusha, hicho kikombe kilichojaa makali yangu hutakinywa tena. Sasa nitakitia mikononi mwao waliokutesa, waliokuambia: Lala chini, tupite juu yako! nawe hukuwa na budi kitumia migongo yako kuwa nchi, kuwa njia ya kupitia hapohapo. Amka! Amka! Ivae nguvu yako, Sioni! Zivae nguo zako tukufu, Yerusalemu, ulio mji mtakatifu! Kwani mwako hatamwingia tena asiyetahiriwa wala mwenye uchafu. Yakung'ute mavumbi, kisha inuka, upate kukaa, Yerusalemu! Yafungue mafungo yaliyopo shingoni pako, binti Sioni, uliofungwa! Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mliuzwa bure, kwa hiyo hamtakombolewa kwa fedha. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Misri ndiko, walikotelemkia kwanza walio ukoo wangu, wakae huko; lakini Waasuri wamewakorofisha bure. Sasa inakuwaje? Ninapata nini hapo? ndivyo, asemavyo Bwana. Walio ukoo wangu wamechukuliwa bure, nao wanaowatawala hulia kwa furaha, tena siku zote Jina langu hutukanwa; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwa sababu hii walio ukoo wangu na walijue Jina langu, kweli siku ile watajua, ya kuwa mimi ndimi nisemaye: Nitazameni, nipo! *Tazameni, miguu yake mpiga mbiu njema jinsi inavyopendeza milimani, anapotangaza utengemano, anapopiga mbiu ya mambo mema, anapotangaza wokovu, anapouambia Sioni: Mungu wako ni mfalme! Zisikilize sauti za walinzi wako! Wamepaza sauti pamoja na kupiga shangwe, kwani wanaona na macho yao, Bwana akirudi Sioni. Pigeni shangwe na kupaza sauti, ninyi mabomoko ya Yerusalemu! Kwani Bwana amewatuliza mioyo walio ukoo wake, akaukomboa Yerusalemu. Mkono wake mtakatifu Bwana ameuvua nguo machoni pa makabila yote ya watu, mapeo yote ya nchi yauone wokovu wa Mungu wetu.* Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa! Msiguse yenye uchafu! Tokeni humu kati! Jitakaseni, ninyi mnaovichukua vyombo vya Bwana! Kwani hamtatoka upesiupesi, wala hamtakwenda na kukimbia, kwani atakayewaongoza ni Bwana, naye atakayewakusanya nyuma ni Mungu wa Isiraeli. Mtazameni mtumishi wangu, jinsi atakavyoendelea kwa welekevu: atatukuka na kukwezwa, awe mkuu kabisa! Kama wengi walivyokustuka, watamstuka naye: kwa kuwa walipomtazama alikuwa amenyongeka kuliko watu, nalo umbo lake halikuwa kama la wana wa watu; ndivyo, atakavyoshangaza makabila mengi ya watu, nao wafalme wafumbe vinywa vyao kwa ajili yake yeye; kwani watakaomwona ndio wasioambiwa Neno lake, nao wasiolisikia watalijua maana. *Yuko nani anayeutegemea utume wetu? Yuko nani aliyefumbuliwa, mkono wake Bwana unayoyafanya? Alikua machoni pake kama mche, kama chipuko la shina lililoko katika nchi kavu, hakuwa mwenye uzuri wala mwenye utukufu wa mwili, tulipomtazama, hakuna umbo lililotupendeza. Akabezwa, akaachwa na watu, akajulikana kuwa mwenye maumivu, akabezwa kama mtu, watu wanayemfichia nyuso zao, tukamwazia kuwa si kitu. Kumbe ameyachukua manyonge yetu, akajitwisha maumivu yetu, nasi tukamwazia kwamba: Ameteswa na Mungu, akapigwa naye, anyongeke. Kumbe ilikuwa kwa ajili ya mapotovu yetu, akichomwa, akaumizwa kwa ajili ya manza zetu, tulizozikora sisi; akapatilizwa, sisi tupate kutengemana, namo katika mavilio yake ndimo, tulimoponea. Sote tulikuwa tumepotea kama kondoo, kila mtu akiishika njia yake, naye Bwana akampigia manza, tulizozikora sisi wote. Alipoonewa yeye amevumilia tu, hakukifumbua kinywa chake kama kondoo, akipelekwa kuchinjwa; au kama mwana kondoo anavyowanyamazia wenye kumkata manyoya, hakukifumbua kinywa chake. Ameuawa kwa kusongwa na kwa kunyimwa uamuzi mnyofu, lakini kwao wa kizazi chake yuko nani ayawazaye kwamba: Ameondolewa katika nchi yao walio hai, alipopigwa kwa ajili ya upotovu wao walio ukoo wake? Wakampa kaburi lake pamoja nao wasiomcha Mungu, alipokwisha kufa akazikwa pake mwenye mali, naye hakufanya ukorofi, uwongo tu haukuonekana kinywani mwake. Lakini Bwana alipendezwa na kumwumiza, asipone, kwamba: Atakapojitoa kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi kwa ajili ya makosa ya watu, ndipo, atakapopata mazao, ndipo, siku zake zitakapoanzia kuwa nyingi, nayo yampendezayo Bwana yatatimizwa na mkono wake. Kwa kuwa roho yake imesumbuliwa, na aone mapato ya kumshibisha; naye alivyo mtumishi wangu mwongofu, ndivyo, atakavyopatia wengi wongofu kwa ujuzi wake, kwani amejitwisha manza zao, walizozikora. Kwa hiyo nitamgawia wengi, wawe fungu lake, naye atawagawia wanguvu mateka yao, yawe mafungu yao, kwa kuwa ameimwaga roho yake, ife, akahesabiwa kuwa mwenzao wapotovu. Naye ameyachukua makosa ya watu wengi, akawaombea nao wapotovu.* Shangilia, wewe uliye mgumba, usiyezaa! Jichekelee na kupaza sauti, wewe usiyeona uchungu wa kuzaa! Kwani wana wake yule aliye peke yake ni wengi kuliko wana wake yule aliye na mumewe; ndivyo, Bwana anavyosema. Papanue mahali pa hema lako! Nazo nguo za hema za makao yako na waziwambe na kuzivuta! Usiwazuie! Kamba za hema ziongeze, ziwe ndefu! Mambo zake zipigilie, zishike vema! Kwani utazieneza pande za kuumeni nazo za kushotoni, nao wazao wako watatwaa makabila ya watu, wakae katika mahame ya miji yao. Usiogope! Kwani hutapatwa na soni, wala hutaiva uso, kwani hutadanganyika, kwa kuwa utazisahau soni, ulizoziona ulpokuwa kijana, nayo matusi, uliyotukanwa ulipokuwa mjane, hutayakumbuka. Kwani mumeo ni yeye aliyekufanya, Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake, naye mkombozi wako ni Mtakatifu wa Isiraeli aitwaye Mungu wa nchi zote. Kwani ulipokuwa mwanamke aliyeachwa, aliyesikitika rohoni, Bwana alikuita. Naye mke wa ujana anakataliwaje? Ndivyo, Mungu wako anavyosema. Kweli kitambo kidogo nimekuacha, lakini nitakupokea tena kwa huruma kubwa. Makali yalipofurika, nimeuficha uso wangu punde kidogo, usiuone, lakini kwa upole ulio wa kale na kale nitakuhurumia; ndivyo, Bwana aliye mkombozi wako anavyosema. Hayo yatakuwa, kama yalivyokuwa katika mafuriko ya Noa, nikaapa: Mafuriko ya Noa hayataididimiza nchi tena; vivyo hivyo nimeapa sasa kwamba: Sitakutolea makali tena, wala sitakukaripia. Ijapo milima iondoke, ijapo navyo vilima vitikisike, upole wangu hautaondoka kwako, wala agano la utengemano wangu halitatikisika; ndivyo, Bwana akuhurumiaye anavyosema. Kweli umenyongeka kwa kutikiswa na upepo mkali, hukutulizwa moyo! Lakini na uone, mimi ninavyokujenga na kuyaweka mawe yako katika udongo wenye wanja na kuitengeneza misingi yako kwa mawe ya safiro. Minara yako nitaijenga kwa mawe ya yaspi, nayo malango yako kwa mawe yamulikayo, nalo boma lako zima kwa mawe ya vito vizuri. Watoto wako wote watakuwa wamefundishwa na Bwana, hivyo watoto wako watakuwa wametengemana kabisa. Wongofu wao utakuwa nguvu zako; kwa hiyo jitenge na ukorofi! Kwani hakuna kitakachokuogopesha. Acha kustuka! Kwani hakuna tisho litakalokufikia. Kama wanakujia, si kwa kuagizwa na mimi; kwa hiyo yuko nani atakayekujia, akupige? Hapo atakapopigana na wewe ataanguka. Tazameni! Mimi nimeumba mafundi wanaowakisha moto wa makaa, watengeneze mata ya kufanyia kazi zao; tena mimi ndiye niliyeumba nao waangamizi wa kuyavunja. Hakuna mata yatakayozimaliza kazi zao yakiwa yametengenezwa ya kukuumiza, nao kila ulimi utakaokuinukia shaurini utashinda na kuupatilizia mabaya; hilo ndilo fungu, watumishi wake Bwana watakalolitwaa, hilo ndilo pato la wongofu wao, nitakalowapatia; ndivyo, asemavyo Bwana. Nyote mwonao kiu, njoni kwenye maji! Nanyi mkosao fedha, njoni kununua, mpate kula! Nunueni pasipo fedha bure tu mvinyo na maziwa! Mbona mnatoa fedha pasipo kupata chakula? Nayo mapato yaliyowachokesha mbona mnayatoa pasipo kushiba? Nisikilizeni, mpate kula mema, roho zenu zipendezwe na manono! Yategeni masikio yenu! Njoni kwangu, mnisikie, roho zenu zipate kupona! Nami nitafanya nanyi agano la kale na kale la kuwapa magawio ya Dawidi yanayotegemeka. Jueni! Nimemweka kunishuhudia kwa makabila ya watu, akawa mkuu na mtawala makabila ya watu. Tazama! Utaita watu, usiowajua, nao watu wasiokujua watakukimbilia, kwa kuwa uko na Bwana Mungu wako, kwa kuwa Mtakatifu wa Isiraeli amekupa utukufu. *Mtafuteni Bwana, akingali yuko, aoneke! Mwiteni, akingali karibu! Asiyemcha Mungu na aiache njia yake, kila mtu na auache upotovu wa mawazo yake! Na arudi kwake Bwana Mungu wetu, amhurumie! Kwani huzidisha kutuondolea mabaya. Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Mawazo yangu siyo mawazo yenu, wala njia zenu sizo njia zangu; kama mbingu zilivyo juu kabisa kuliko nchi, ndivyo, njia zangu zilivyo juu kabisa kuliko zenu, ndivyo, nayo mawazo yangu yalivyo makuu kuliko mawazo yenu. Kwani kama mvua ya maji na ya mawe inavyoshuka toka mbinguni, isirudi huko, isipokwisha kuinywesha nchi na kuizalisha na kuichipuza, itoe mbegu za kupanda na vilaji vya kula: ndivyo, litakavyokuwa Neno langu litokalo kinywani mwangu, nalo halitarudi kwangu bure lisipokwisha kufanya yanipendezayo, lipate kuyatimiza, ambayo nililituma kuyafanya.* Kwani mtatoka na kufurahi, mtaongozwa, mwende na kutengemana. Milima navyo vilima vitapaza sauti za kushangilia mbele yenu, hata miti yote ya porini itapiga makofi. Palipokuwa na mikunju tu, patakuwa na mivinje, napo palipokuwa na viwawi tu, patakuwa na miti ya vihagilo, nayo miti hiyo italitangaza Jina la Bwana, iwe kielekezo chake cha kale na kale kisichong'oleka. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Yaangalieni yapasayo, myafanye yaongokayo! Kwani wokovu wangu uko karibu, utokee, nao wongofu wangu na ufunuliwe. Mwenye shangwe ni mtu atakayeyafanya naye mwana wa mtu atakayeyashika, anayeziangalia siku za mapumziko, asizichafue, anayeiangalia mikono yake, isifanye kibaya cho chote. Naye mwana wa nchi ngeni aliyeandamana na Bwana asiseme: Bwana atanitenga kabisa kwao walio ukoo wake! Wala aliyekatazwa kuzaa asiseme: Nitazameni, mimi ni mti mkavu! Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Waume wasiozaa kama wanazingalia siku zangu za mapumziko, kama wanayachagua yanipendezayo, walishike sana Agano langu, nitawapa nyumbani mwangu na bomani kwangu mahali, ndipo majina yao yakae, napo patakuwa pema kuliko pengine penye wana wa kiume na wa kike; kweli nitawapa majina ya kale na kale yasiyong'oleka. Nao wana wa nchi ngeni walioandama na Bwana, wamtumikie, walipende Jina lake Bwana, wawe watumishi wake, wote waziangaliao siku zake za mapumziko, wasizichafue, walishike Agano lake, hawa nitawapeleka kwenye mlima wangu mtakatifu, niwafurahishe Nyumbani mwangu mwa kuombea, nazo ng'ombe zao za tambiko na vipaji vyao vingine vya tambiko vitanipendeza vitakapotolewa mezani pangu pa kunitambikia, kwani Nyumba yangu itaitwa nyumba ya kuombea kwao makabila yote ya watu. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu anayewakusanya Waisiraeli waliotawanyika: Wako wengine wa kwao, nitakaowakusanya, niwatie kwao waliokusanywa. Ninyi nyama wa porini nyote, nanyi nyama wa mwituni, nyote njoni, mle! Walinzi wa watu wangu ni vipofu wote, hawajui kitu; wote ni mbwa mabubu wasioweza kulia, hulala na kuota ndoto, hupenda kupumzika tu. Tena ni mbwa walafi wasiojua kushiba; hawa walio wachungaji hawajui kitu, wala hawatambui maana, wote wamezishika njia zao, kila hutaka kupata tu, hakuna asiye hivyo. Husema; Njoni, nichukue mvinyo, tunywe, hata tutakapolewa! Vivyo hivyo itakuwa nayo siku ya kesho, iwe sikukuu kabisa kupita cheo. Mwongofu akiangamia, hakuna aumiaye moyoni; wapole wakiondolewa, hakuna ayatambuaye, ya kuwa mwongofu huondolewa, ubaya ulipo. Nao huingia kwenye utengemano, hupumzika hapo, wanapolala wao waliozifuata njia zao zinyokazo. Nanyi karibuni hapa, mlio wana wa mwaguaji wa kike! Mlio uzao wa mvunja unyumba na mwanamke mgoni! Yuko nani, mnayemcheka? Yuko nani, mnayemwasamia vinywa na kutoa ndimi? Je? Ninyi ham wana wa upotovu na mazao ya uwongo? Mnaingiwa na tamaa chini ya mitamba napo chini ya kila mti wenye majani meusi, mnachinja watoto mitoni kwenye mapango ya miamba. Mawe ya mtoni yatelezayo na fungu lako, hayo ndiyo, unayoyatumia kuwa kura yako; nayo huyamwagia vinywaji vya tambiko, ukayatolea hata vilaji vya tambiko. Sasa je? Hayo niyanyamazie tu? Kwenye mlima mrefu juu kileleni hujitandikia pako pa kulalia, ukipanda huko kuchinja ng'ombe za tambiko. Kwa kuniacha mimi unakiweka kinyago chako cha nyumbani nyuma ya mlango kwenye miimo; kisha ukakifunua kilalo chako, ukakipanda, ukakipanua, ukajichagulia mmoja wao, ukapenda kulala nao, ulipoona mkono uliokupungia. Ukasafiri kumwendea mfalme ukichukua mafuta ya kukipaka na manukato yako mengi, ukatuma wajumbe wako kwenda katika nchi za mbali, ukawaendesha hata kushuka kuzimuni. Ukachoka kwa njia zako nyingi, lakini hukusema: Tamaa zimekatika; ulipoona mkononi mwako, ya kuwa nguvu zimo bado, basi, hukulegea. Ni kwa ajili ya nani ukitishika, ukamwogopa, ukafanya ya uwongo? Lakini mimi hukunikumbuka, hukuniweka moyoni mwako. Imekuwaje? Sivyo hivyo: kwa kuwa mimi nimenyamaza tangu kale, hukuniogopa? Nami na nitangaze, wongofu wako ulivyo, lakini viumbe vyako havitakufalia kitu. Utakapolia, na vikuponye vile vyote, ulivyovikusanya! Lakini hivyo upepo utavichukua, pumzi tu itaviondoa. Naye anikimbiliaye ataitwaa nchi, nao mlima wangu mtakatifu ataupata kuwa wake. Amesema: Chimbeni! Chimbeni! Itengenezeni njia! Yaondoeni makwazo njiani kwao walio ukoo wangu! Kwani hivi ndivyo, anavyosema atukukaye, Alioko huko juu, akaaye kale na kale, aitwaye jina lake Mtakatifu: Ninakaa hapa juu patakatifu, tena kwao wapondekao na kunyenyekea rohoni, nizirudishe uzimani roho zao wanyenyekevu, niirudishe uzimani nayo mioyo yao wapondekao. Kwani sitagomba kale na kale, wala sitakasirika siku zote, roho zao zisizimie mbele yangu pamoja nao wenye pumzi, niliowafanya mimi. Ubaya wa choyo chao niliukasirikia, nikawapiga nikijificha kwa kuwa na makali, nao wakajiendea na kuniacha, wakashika njia za kuipendeza mioyo yao. Nikaziona hizo njia zao, kwa hiyo nitawaponya na kuwaongoza, niwalipe na kuwatuliza mioyo wao na wenzao, waliowasikitikia. Na niumbe mazao ya midomo itakayotangaza utengemano kwamba: Utengemano utawajia walioko mbali nao walioko karibu! Ndivyo, anavyosema Bwana: Kweli nitawaponya. Lakini wasiomcha Mungu hufanana na bahari ichafukayo, isiyoweza kutulia kamwe, mawimbi yake hayakomi kutoa machafu na takataka. Hakuna utengemano kwao wasiomcha Mungu; ndivyo, anavyosema Mungu wangu. Ita kwa kinywa kikuu! Usijizuie! Paza sauti yako, kama ni baragumu! Walio ukoo wangu watangazie mapotovu yao! Walio mlango wa Yakobo watangazie makosa yao! Kweli siku kwa siku hunitafuta, hutaka kuzijua njia zangu, kama ni watu wafanyao yaongokayo, kama ni watu wasioyaacha yampasayo Mungu wao; wakaniuliza mashauri yaongokayo wakinitaka mimi Mungu, niwafikie karibu. Husema: Mbona huoni, tukifunga mifungo? Mbona hujui, tukizisumbua roho zetu? Lakini tazameni: Siku mnapofunga hufuata mambo, myapendayo, nao wakazi wenu huwashurutisha kuja kazini. Tazameni: Mnapofunga hugombana na kutetena, mkapigana makonde, kwani hammchi Mungu, hamfungi kwamba: Ni siku ya kumlilia Alioko huko juu. Je? Huo ndio mfungo, nilioupenda, uwe siku, mtu anapojinyima yamfaayo? Mtu akikiinamisha kichwa chake kama unyasi, tena akilalia gunia na majivu,, huo utauita mfungo na siku ya kumpendeza Bwana? Je? Mfungo, nilioupenda sio huu: kufungua mafungo ya ukorofi, kulegeza kamba za utumwa, kuwapa ruhusa waliopondeka, wajiendee, kuvunja utumwa wo wote? Sivyo hivyo? Ukimgawia mwenye njaa mkate wako. ukiingiza nyumbni mwako wakiwa waliofukuzwa, unapoona mwenye uchi ukimpa nguo, usipowakataa walio wa mlango wako? Ukifanya hivyo, ndipo, mwanga wako utakapopambazuka kama mionzi ya jua, ndipo, vidonda vyako vitakapopona upesi, ndipo, wongofu wako utakapokutangulia, nao utukufu wa Bwana utakufuata nyuma. Ndipo, itakapokuwa hivyo: utakapoita, Bwana atakuitikia; utakapolia, atakuambia: Mimi hapa! Lakini kwanza sharti uondoe utumwa katikati yako, uache kunyoshea watu vidole na kusema maovu. Mwenye njaa utakapompa, roho yako iyatakayo nayo, utakapoishibisha roho ya mkiwa, ndipo, mwanga wako utakapotokea gizani, ndipo, weusi wa usiku utakapokuwa kwako kama jua la mchana. Naye Bwana atakuongoza siku zote, aishikize roho yako katika nchi kavu; nayo mifupa yako ataishupaza, uwe kama shamba lililonyweshwa au kama kisima cha maji kisichodanganya kwa kuwa na maji yasiyokauka. Nao watakaotoka kwako watayajenga mabomoko yako ya kale, nayo misingi ya vizazi na vizazi utaitengeneza tena; kwa hiyo watakuita: Mjenga nyufa na Mfufua njia, watu wakae. Kama utaikataza miguu yako siku za mapumziko, isifanye penye siku yangu takatifu yakupendezayo, kama siku ya mapumziko utaiita ya kupendezwa, kwa kuwa ni siku ya Bwana mtakatifu ipasayo kutukuzwa, ukaitukuza na kuacha kuzishika njia zako, usipoyafuata uyapendayo, usipojisemea maneno tu: ndipo, utakapopendezwa na Bwana, nami nitakupitisha kwenye vilima vya nchi, kisha nitakupa nalo fungu la baba yako Yakobo, ulile, kwani kinywa chake Bwana kimeyasema. Tazameni: Mkono wake Bwana sio mfupi, usiweze kuokoa, wala masikio yake siyo mazito, yasiweze kusikia. Ila manza zenu, mlizozikora, ndizo zinazowatenga ninyi na Mungu wenu, nayo makosa yenu ndiyo yanayowafichia uso wake asiwasikie. Kwani mikono yenu imechafuliwa na damu, hata vidole vyenu vimechafuliwa na mabaya, viliyoyafanya; midomo yenu husema uwongo, ndimi zenu hunong'ona mapotovu. Hakuna amwitaye mwenziwe shaurini kwa kuyataka yaongokayo, wala hakuna ahukumuye kwa kweli, huyakimbilia yaliyo maovyo tu, hujisemea yasiyo maana, huchukua mimba ya maumivu, huzaa mapotovu. Huangua mayai ya pili, hufuma matandabui; mtu akiyala mayai yao hufa, nalo lipasukalo hutoka nyoka. Matandabui yao hayatumiki kuwa mavazi, hawawezi kujifunika kwa hizo kazi zao; kazi zao ni kazi za upotovu, matendo ya ukorofi yamo mikononi mwao. Miguu yao hukimbilia mabaya, hupiga mbio kuja kumwaga damu zao wasiokosa, mawazo yao ni mawazo mapotovu, maangamizo na mavunjiko huzijulisha njia zao. Lakini njia ya utengemano hawaijui, wala maamuzi yapasayo hayako kwenye mapito yao, mikondo yao wameipotoa, wote waifuatao hawajui utengemano. Kwa sababu hii maamuzi yapasayo yametukalia mbali, nayo yaongokayo hayafiki kwetu. Tukangojea, kuche, lakini tunaona giza tu, tukangojea, kupambazuke, lakini vivyo hivyo tunajiendea na weusi wa usiku. Tunapapasa ukutani kama vipofu, kweli tunapapasa tu kama watu wasio na macho; tunajikwaa na mchana, kama ni jioni, tuko kama wafu kwao walio wenye nguvu. Sisi sote huvuma kama nyegere, hulia, kama hua wanavyolia, tukayangojea yale maamuzi yapasayo, lakini hayako, tukaungojea wokovu, nao ukawa mbali, usifike kwetu. Kwani mapotovu yetu yako mengi mbele yako, nayo makosa yetu yanatusuta; kwani mapotovu yetu yako kwetu, nazo manza zetu tunazijua. Tumemtengua Bwana na kumkana, tukarudi nyuma na kumwacha Mungu wetu, tukasema maoneo na machokozi, tukachukua maneno ya uwongo kama mimba, tukayatoa tena mioyoni. Kwa hiyo maamuzi yapasayo yamerudishwa nyuma, nayo yaongokayo yakasimama mbali; kwani ya kweli yalijikwaa njiani, nayo yaliyo sawa hayakuweza kuingia. Kwa hiyo kweli ikakosekana, naye aliyeacha mabaya hunyang'anywa. Bwana alipoyaona, yakawa mabaya machoni pake, kwa kuwa hakuna maamuzi yapasayo. Akaona, ya kuwa hakuna mtu, akashangaa, ya kuwa hakuna msaidiaji; ndipo, mkono wake ulipomtumikia kuwa wa kuokoa, nao wongofu wake ukamshikiza. Akajivika wongofu kuwa fulana ya chuma kifuani, kichwani akavaa wokovu kuwa kofia, kisha akajivika lipizi kuwa mavazi ya mwili, akajifunika wivu kuwa nguo za juu. Kama matendo yao yalivyo, ndivyo, nayo malipizi yatakavyokuwa: makali yatawatokea waliompingia, nao waliomchukia watafanyiziwa vivyo hivyo, hata visiwa atavilipisha matendo yao. Hapo ndipo, watakapoliogopa Jina la Bwana machweoni kwa jua, nako maawioni kwa jua watauogopa utukufu wake, kwani atakuja kama mto unaopita mahali pembamba, upepo wa Bwana ukiyasukuma maji yake. Sioni ataingia atakayewakomboa wa Yakobo walioyaacha mapotovu; ndivyo, asemavyo Bwana. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Hili ni agano langu mimi, ninalolifanya nao: Roho yangu inayokukalia na maneno yangu, niliyoyatia kinywani mwako, hayataondoka kinywani mwako, wala vinywani mwao walio wa uzao wako, wala mwao walio uzao wa uzao wako, kuanzia sasa hata kale na kale; ndivyo, Bwana anavyosema. *Inuka uangazike! Kwani mwanga wako unakuja, nao utukufu wa Bwana umekuzukia. Kwani tunapotazama, giza linaifunika nchi, mawingu meusi yanayafunika makabila ya watu, lakini wewe, Bwana anakuzukia, nao utukufu wake unaonekana juu yako. Wamizimu wataujia mwanga wako, nao wafalme wataujia mmuliko uliozuka kwako. Yainue macho yako, utazame po pote! Hao wote wamekusanyika, waje kwako; wanao wa kiume watakuja, wakitoka mbali, wanao wa kike wataletwa na kubebwa. Utakapowaona utachangamka, nao moyo wako utapigapiga, upanuke, kwani mafuriko ya bahari yatageuka, yaje kwako, nayo mapato ya wamizimu yataingia kwako. Makundi ya ngamia yatakufunika, hata vijana wa ngamia wa Midiani na wa Efa, wote watatoka Saba, waje kwako, wakichukua dhahabu na uvumba, nao watamtangaza Bwana na kumshangilia.* Makundi yote ya Kedari, yale ya mbuzi na ya kondoo yatakusanyika kwako, madume ya Nebayoti utayatumia ya tambiko, yatanipendeza juu ya meza ya kunitambikia; ndivyo, nitakavyoitukuza Nyumba ya utukufu wangu. Hao ni wa nani wanaoruka kama mawingu au kama hua wanaoyarukia matundu yao? Kwani visiwa vinaningojea, nazo merikebu za Tarsisi zitakuwa za kwanza za kuwaleta wanao toka nchi za mbali; fedha zao na dhahabu zao wanazo za kulitolea Jina la Bwana Mungu wako, kwa kuwa yeye aliye Mtakatifu wa Isiraeli amekupa utukufu. Wana wa nchi ngeni watalijenga boma lako, nao wafalme wao watakutumikia, kwani nilipokuchafukia nilikupiga, tena nilipopendezwa nawe nimekuhurumia. Malango yako yatakuwa wazi siku zote, hayatafungwa mchana wala usiku, wakuletee mapato ya wamizimu, nao wafalme wao watajitia mumo humo. Kwani kila taifa na kila nchi ya kifalme itakayokataa kukutumikia itaangamia, nao watu wao watatoweka kabisa. Utukufu wa Libanoni utakuja kwako, mivinje na mitamba na mizambarau yote pamoja iwe mapambo ya mahali pangu patakatifu, maana mahali, miguu yangu itakapopakanyaga, nitapapatia marembo. Nao wana wao waliokutesa watakuja kwako na kuinama chini, nao wote waliokutukana watakuangukia penye nyayo za miguu yako, watakuita mji wa Bwana, Sioni wa Mtakatifu wa Isiraeli. Kwa sababu ulikuwa umeachwa, ukachukizwa, watu wakakataa kupitia kwako, kwa hiyo nitakuweka kuwa mahali pa kujivunia kale na kale, tena kuwa wa kufurahisha vizazi na vizazi. Utanyonya maziwa ya mataifa mengine, kweli vifuani kwa wafalme utanyonya, kwani mimi Bwana ni mwokozi wako, mkombozi wako ni yeye amtawalaye Yakobo. Penye shaba nitaleta dhahabu, penye vyuma nitaleta fedha, penye miti nitaleta shaba, penye mawe nitaleta vyuma. Nitaweka utengemano kuwa ukuu wako nao wongofu kuwa ubwana wako. Hayatasikiwa tena makorofi katika nchi yako, wala hayatasikilika maangamizo na mavunjiko katika mipaka yako. Boma lako utaliita Wokovu, nayo malango yako utayaita Mashangilio. Halitawaka tena jua kwako kuwa mwanga wa mchana, wala mwezi hautakumulikia tena, upate kuona, kwani Bwana atakuwa mwanga wako kale na kale, Mungu wako atakuwa utukufu wako. Jua lako halitakuchwa tena, wala mwezi wako hautakufa tena, kwani Bwana atakuwa mwanga wako wa kale na kale, nazo siku zako za kusikitika zitakuwa zimekwisha. Walio wa ukoo wako wote watakuwa waongofu, watakuwa wenye nchi kale na kale, kwa kuwa ni shamba, nililolipanda, ni kazi ya mikono yangu, nijipatie matukuzo. Aliye mdogo atageuka kuwa elfu, naye aliye mnyonge atageuka kuwa taifa lenye nguvu. Mimi Bwana nitayafanyiza upesi, siku zake zitakapotimia. *Roho ya Bwana Mungu inanikalia, kwa hiyo Bwana amenipaka mafuta, niwapigie maskini mbiu njema. Amenituma, niwaponye waliovunjika mioyo, niwatangazie mateka, ya kuwa watakombolewa, nao waliofungwa, ya kuwa watatolewa mafungoni, niutangaze mwaka wa Bwana upendezao na siku ya lipizi ya Mungu wetu, niwatulize mioyo wote wasikitikao, niwapoze mioyo yao wausikitikiao Sioni, nikiwapa vilemba penye majivu na mafuta ya furaha penye mavazi ya matanga na mashangilio penye roho za kuzimia, watu wawaite Mivule iongokayo na Shamba la Bwana la kujipatia matukuzo. Watayajenga mabomoko yako ya kale, nayo mahame ya siku za mbele watayasimamisha tena, nayo miji iliyo machungu ya mawe tu watairudishia upya, ndiyo iliyokuwa imeangamia kwao vizazi na vizazi. Wageni watasimama hapo wakiyachunga makundi yenu, waliotoka nchi nyingine watakuwa wakulima wenu na watunza mizabibu yenu. Nanyi mtaitwa watambikaji wa Bwana, mtaambiwa: M watumishi wa Mungu wetu; mapato ya wamizimu mtayala, nayo matukufu yao yatakuwa mali zenu.* Penye soni walizotiwa watapata malipo mara mbili, penye matusi watalishangilia fungu lao. Kweli katika nchi yao watakuwa wenye mafungu mawili, tena watapata kuchangamka kale na kale. Kwani mimi Bwana ninapenda maamuzi yapasayo, nikachukiwa nayo yaliyopokonywa kwa upotovu, kwa hiyo nitawapa kwa kweli yayapasayo matendo yao, nitafanya nao agano la kale na kale. Mazao yao yatajulikana kwa wamizimu, nao waliotoka miilini mwao watajulikana katikati ya makabila ya watu; wote watakaowaona watawatambua, ya kuwa ndio mazao yaliyobarikiwa na Bwana. Kufurahi nitamfurahia Bwana, roho yangu itampigia Mungu wangu shangwe, kwani amenivika mavazi ya wokovu, akanifunika kwa kanzu ya wongofu, niwe kama mchumba mume, akiutengeneza urembo wa kichwani kuwa kama wa mtambikaji, au kama mchumba mke, akijipamba na kuvaa vito vyake. Kwani kama nchi inavyoyatoa machipukizi yake, kama shamba linavyozichipuza mbegu zake, ndivyo, Bwana Mungu atakavyochipuza wongofu na mashangilio mbele ya wamizimu wote. Kwa ajili ya Sioni sitanyamaza, kwa ajili ya Yerusalemu sitapumzika, mpaka yaupasayo yatokee kama mwangaza, mpaka wokovu wake uwe kama mwenge uwakao. Ndipo, wamizimu watakapoona yaliyokupasa, nao wafalme wote watauona utukufu wako, nawe utaitwa kwa jina jipya, kinywa cha Bwana kitakalolitaja. Ndipo, utakapokuwa urembo wa kichwa wenye utukufu mkononi mwa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako. Hutaambiwa tena: Umeachwa! Wala nchi yako haitaambiwa tena: Ni pori tupu, ila utaitwa: Hunipendeza, nayo nchi yako itaitwa: Ameolewa, kwani Bwana atapendezwa na wewe, nayo nchi yako itaolewa. Kwani kama mchumba mume anavyomchukua mwali, ndivyo, wanao watakavyokuchukua wewe, kama mwenye ndoa anavyomfurahia mchumba wake, ndivyo, Mungu wako atakavyokufurahia. *Bomani kwako, Yerusalemu, nimeweka walinzi juu, mchana kutwa na usiku kucha wasinyamaze kamwe. Ninyi mnaolitangaza Jina la Bwana, msiwe kimya! Wala msimwache Bwana kuwa kimya, mpaka aushikize Yerusalemu tena na kuuweka, utukuzwe katika nchi! Bwana ameapa na kuutaja mkono wake wa kuume ulio na nguvu kwamba: Sitazitoa tena ngano zako, ziliwe na adui zako, wala wana wa nchi ngeni wasinywe tena pombe zako, ulizozisumbukia. Ila watakaozivuna ndio watakaozila, wamshukuru Bwana, nao watakaozichuma ndio watakaozinywa nyuani penye Patakatifu pangu. Piteni mlangoni, mwitengeneze njia yao walio ukoo wetu! Chimbeni! Ichimbeni barabara na kuyaondoa mawe! Twekeni bendera, makabila ya watu yaione! Angalieni! Bwana anatangaza mapeoni kwa nchi kwamba: Mwambieni binti Sioni: Tazama, wokovu wako unakuja! Tazama, mshahara wake wa kulipa anao, nayo mapato yake yako mbele yake. Nao watawaita: Ukoo mtakatifu ulio wao waliokombolewa na Bwana, nawe utaitwa Mji uliotafutwa, usioachwa tena.* Ni nani huyu anayetoka Edomu na kuvaa nguo nyekundu za Bosira? Ni mtukufu katika vazi lake, anatembea na kuzionyesha nguvu zake nyingi; anasema: Yuko nani asemaye kwa wongofu? Ninazo njia nyingi za kuokoa. Mbona vazi lako ni jekundu? Mbona nguo zako zinafanana nazo za mkamua zabibu? Kweli nimekamua kamulioni mimi peke yangu, pasipokuwa na mtu mwingine, nikawakamua kwa makali yangu, nikawaponda kwa moto wa machafuko yangu, damu zao zikazirukia nguo zangu, nikayachafua mavazi yangu yote, kwani ilikuwa siku ya lipizi, niliyoiweka moyoni mwangu, tena umetimia mwaka wa kuwakomboa walio wangu. Nikatazama, lakini hakuna msaidiaji, nikachungulia na kushangaa, lakini hakuna ashikizaye; ndipo, mkono wangu uliponitumikia kuwa wa kuokoa, nao moto wa machafuko yangu ukanishikiza. Basi, nikayoponda makabila ya watu kwa makali yangu, nikawalevya kwa moto wa machafuko yangu nilipozimwaga damu zao chini. *Nitawakumbusha magawio ya Bwana na kumtukuza Bwana kwa ajili yao yote, aliyotutendea Bwana; mema yake ni mengi, aliyoutendea mlango wa Isiraeli kwa huruma zake aliwagawia mengi. Akasema: Kumbe hawa ndio walio ukoo wangu, ndio wanangu, hawataongopa; akawa mwokozi wao. Katika masongano yao yote naye alikuwa amesongeka; ndipo, malaika aliyetoka usoni kwake alipowaokoa, kwa kuwapenda na kwa kuwaonea uchungu akawakomboa yeye mwenyewe, akawaokota, akawachukua siku zote za kale. Lakini wakaacha kumtii, wakaisikitisha Roho yake takatifu; ndipo, alipogeuka kuwa adui yao, akapigana nao mwenyewe. Ndipo, wao walio ukoo wake walipozikumbka siku za kale, siku za Mose, wakasema: Yuko wapi aliyewatoa baharini pamoja na mchungaji wa kundi lake? Kwa mkono wake wenye utukufu alimwongoza Mose alipomshika mkono wake wa kuume, akayatenga maji mbele yao, ajipatie Jina la kale na kale. Akawapitisha vilindini kama farasi nyikani, wasijikwae. Kama kundi linavyotelemka bondeni, ndivyo, roho ya Bwana ilivyowapeleka pa kupumzikia. Hivyo ndivyo, ulivyowaongoza walio ukoo wako, ujipatie Jina lenye utukufu. Chungulia toka mbinguni! Tazama toka Kao lako takatifu lenye utukufu! Wivu wako uko wapi? Matendo yako ya nguvu yako wapi? Huruma zako zinazovuma moyoni mwako zimejizuia, zisifike kwangu. Kwani wewe ndiwe baba yetu; kwani Aburahamu hakutujua, wala Isiraeli hakututambua. Wewe Bwana ndiwe baba yetu; Mkombozi wetu ndilo jina lako la kale.* Mbona umetupoteza, Bwana, tukaziacha njia zako? Mbona umeishupaza mioyo yetu, isikuogope? Rudi kwa ajili ya watumishi wako walio milango ya fungu lako! Ilikuwa kitambo kidogo tu, watu wako watakatifu walipokuwa wenye mafungu yao, kisha wao waliotusonga walipaponda Patakatifu pako, tukawa watu, usiowatawala tangu kale, wasiolitambikia Jina lako. Laiti ungizipasua mbingu, ukashuka, milima ikitukutika mbele yako! Kama moto unavyokoleza vijiti, viwake, au kama moto unavyochemsha maji, hivyo wajulishe wapingani wako Jina lako, wamizimu watetemeke mbele yako! Ungefanya matendo yatishayo, tusiyoyangojea, ukashuka, milima ikitukutika mbele yako! Tangu kale hawakusikia, wala hawakupata habari, wala macho hayakuona, ya kuwa yko Mungu anayewafanyia matendo wamngojeao, isipokuwa wewe. Unawaendea wafurahiao kufanya yaongokayo, nao wakukumbukao katika njia zako. Tazama, ulikasirika, tulipokosa na kuendelea hivyo siku nyingi, lakini huko nyuma tukaokolewa. Sisi sote tumekuwa kama wachafu, wongofu wetu wote ukawa kama nguo yenye madoadoa; sisi sote tukanyauka kama majani, mabaya yetu yakatuchukua, kama upepo unavyochukua majani makavu. Hakuna alitambikiaye Jina lako, hakuna ajihimizaye kukushika, kwani umeuficha uso wako, tusiuone, ukatuacha, tuzimie kwa nguvu za manza, tulizozikora. Na sasa, Bwana, wewe ndiwe baba yetu; sisi tu udongo, nawe ndiwe mfinyanzi wetu, sisi sote tu kazi za mikono yako. Bwana, usizidi kukasirika sana, wala usizikumbuke manza kale na kale! Twakuomba: Tutazame! Sisi sote tu ukoo wako! Miji yako mitakatifu imegeuka kuwa mapori, hata Sioni ni pori tupu, Yerusalemu umeangamia. Nyumba yetu takatifu iliyokuwa yenye utukufu, baba zetu walimokushangilia, imeteketezwa na moto; yote, tuliyoyapenda sana, yamegeuka kuwa mabomoko. Bwana, kwa ajili ya hayo utawezaje kujizuia? Utawezaje kunyamaza na kutuacha, tuzidi kunyongeka sana? Nimetafutwa nao wasioniuliza; nimeonwa nao wasioninyatia. Nimewaambia watu wasiolitambikia Jina langu: Mimi hapa! Mimi hapa! Mchana kutwa naliikunjua mikono yangu kuwaita watu wabishi washikao njia isiyo nzuri, wayafuatao mawazo yao. Ndio watu wanaonikasirisha pasipo kukoma, ijapo niwatazame, hutambika shambani, huvukiza kwenye matofali. Hukaa makaburini, hulala usiku penye mwiko, hula nyama za nguruwe, namo vyomboni mwao mna mchuzi wa kibudu. Husema: Jikalie kwako, usinifikie karibu! kwani mimi ni mwiko kwako; hawa ndio wanaotoa moshi puani mwangu, ndio moto uwakao mchana kutwa. Tazameni! Yameandikwa mbele yangu; sitanyamaza, ila nitayalipiza, kweli nitayalipiza vifuani mwao. Manza zenu, mlizozikora, pamoja nazo za baba zenu na mzilipe, ndivyo, Bwana anavyosema; maana wamevukiza milimani juu, nako vilimani juu wamenibeua. Nami kwanza nitawapimia malipo ya matendo yao, wayachukue vifuani mwao. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kama watu wanavyosema fumbo la zabibu, maji yao yakingali yamo, kwamba: Usiziangamize! Kwani mbaraka imo, ndivyo, nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu, nisiwaangamize wote. Nitatokeza mzao kwake Yakobo, nako kwake Yuda atakayekuwa mwenye milima yangu, kusudi wao, niliowachagua, waitwae, watumishi wangu wapate kukaa huko. Nako Saroni kutakuwa na malisho ya makundi ya mbuzi na ya kondoo; nalo bonde la Akori litakuwa pa kukalia ng'ombe kwao walio ukoo wangu, kwa kuwa wamenitafuta. Lakini ninyi mliomwacha Bwana, mkausahau mlima wangu mtakatifu, mkamtandikia meza Mwenye kura, naye Mwenye maaguo mkammiminia vinyweo vilivyojaa mvinyo za tambiko, basi, ninyi nimewaagulia kuuawa kwa panga, nyote mpige magoti, mchinjwe, kwa kuwa nilipowaita, hamkujibu, niliposema, hamkusikia, mkayafanya yaliyokuwa mabaya machoni pangu, mkayachagua, ambayo nilikuwa sipendezwi nayo. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa hiyo na mwone: Watumwa wangu watakapokula, ninyi mtaumwa na njaa; watumwa wangu watakapokunywa, ninyi mtaumwa na kiu; watumwa wangu watakapofurahi, ninyi mtaona soni. Watumwa wangu watakapopiga shangwe kwa kuwa na mema mioyoni, ndipo, ninyi mtakapolia kwa kuumia mioyoni, tena mtapiga makelele kwa kupondeka rohoni. Nayo majina yenu mtayaachilia wao, niliowachagua, watayatumia wakitaka kuapiza na kusema: Bwana Mungu na akuue hivyo! Lakini watumishi wangu atawaita kwa majina mengine. Atakayejiombea mema katika nchi atajiombea kwake Mungu mwenye welekevu, atakayeapa katika nchi ataapa na kumtaja Mungu mwenye welekevu, kwani masongano ya kwanza yatakuwa yamesahauliwa, kwani yatakuwa yametoweka machoni pangu. *Tazameni! Mimi nitaumba mbingu mpya na nchi mpya, nazo za kwanza hazitakumbukwa tena, hazitaingia mioyoni tena. Yafurahieni na kuyashangilia kale na kale, nitakayoyaumba mimi! Kwani na mwone, nikiumba Yerusalemu kuwa pa kushangilia nao watu wake kuwa wenye furaha. Nami nitaushangilia Yerusalemu, nitawafurahia walio ukoo wangu. Mwake hamtasikilika tena sauti za vilio wala sauti za maombolezo.* Hatakuwamo tena mnyonyaji wa siku chache, wala mzee asiyezimaliza siku zake; kwani watakaokufa wakingali vijana watakuwa wa miaka mia, nao watakaokufa wenye miaka mia watawaziwa kuwa wakosaji walioapizwa. Watakaojenga nyumba wataikaa, watakaopanda mizabibu wataila matunda yao. Hawatajenga, mwingine akae humo, wala hawatapanda, mwingine ayale, kwani siku za miti zilivyo, ndivyo, siku zao walio ukoo wangu zitakavyokuwa, nayo, wao niliowachagua watakayoyafanya kwa mikono yao, watayatumia wenyewe. Hawatasumbuka bure, wala hawatazaa watoto watakaogunduliwa na kifo, kwani watakuwa mazao yaliyobarikiwa na Bwana, wao wenyewe nao watakaotoka miilini mwao. *Itakuwa hivyo: Watakapokuwa hawajanililia bado, mimi nitawaitikia; watakapokuwa wanasema bado, mimi nitakuwa nimesikia. Mbwa wa mwitu na mwana kondoo watalisha pamoja, naye simba atakula majani kama ng'ombe, naye nyoka mavumbi yatakuwa chakula chake. Hawatafanya mabaya, wala hawataangamizana katika mlima wangu mtakatifu wote.* Ndivyo, Bwana anavosema. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mbingu ni kiti changu cha kifalme, nayo nchi ni pa kuiwekea miguu yangu. Ni nyumba gani, mtakayonijengea? Tena mahali pa kupumzikia mimi ni mahali gani? Hayo yote mkono wangu uliyafanya, yakawapo hayo yote; ndivyo, asemavyo Bwana. Ninaowatazama, ndio wakiwa nao wapondekao rohoni, nao wanaotetemeka wakalisikia Neno langu. Achinjaye ng'ombe huwa kama mwenye kuua mtu, naye atoaye kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko huwa kama mwenye kunyonga mbwa, naye atoaye vyakula kuwa vipaji vya tambiko humwaga nazo damu za nguruwe, avukizaye uvumba hutambikia mizimu: hao ndio waliojichagulia njia zao, nazo roho zao zikapendezwa na matapisho yao. Ndivyo, nami nitakavyojichagulia masumbufu ya kuwasumbua, nayo matisho, waliyoyaogopa, nitayaleta kwao, kwa kuwa nilipowaita, hawakujibu; niliposema, hawakusikia, wakayafanya yaliyokuwa mabaya machoni pangu, wakayachagua, ambayo nilikuwa zipendezwi nayo. Lisikilizeni Neno la Bwana, mtetemekao mkilisikia Neno la Bwana! Ndugu zenu wanaowachukia ninyi, waliowafukuza kwa ajili ya Jina langu walisema: Bwana na autokeze utukufu wake, tuone, mkiufurahia! Lakini wao watapatwa na soni. Usikilizeni uvumi uliomo mjini, uliomo namo Nyumbani mwa Bwana! Ni sauti ya Bwana anayewalipisha adui matendo yao. Alipokuwa hajashikwa na uchungu bado amezaa, alipokuwa hajaumwa bado amepata mtoto wa kiume. Yuko nani aliyesikia kama hayo? Yuko nani aliyeona kama hayo? Inakuwaje, nchi ikitokezwa siku moja? Inakuwaje, ukoo mzima wa watu ukizaliwa kwa mara moja? Kwani Sioni uliposhikwa na uchungu papo hapo umewazaa watoto wake. Je? Mimi nifikishe watoto pa kuzaliwa, nisiwazalishe? ndivyo, Bwana anavyosema. Je? Mimi ninapozalisha, nilifunge tumbo la mama? ndivyo, Mungu wako anavyosema. Changamkeni pamoja na Yerusalemu! Ushangilieni, nyote mwupendao! Furahini pamoja nao furaha kuu, nyote mliousikitikia! Kwa maana mtayanyonya na kushiba maziwa yake yenye matulizo ya moyo! Kwa maana mtanyonya na kukamua, mjipendezeshe kwa mfuriko wa utukufu wake. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazameni! Nitauelekeza utengemano, ufike kwake ukiwa kama mto mkubwa, nayo matukufu ya wamizimu nitayalekeza, yafike kwake yakiwa kama kijito kifurikacho maji. Nanyi mtanyonya mkibebwa vifuani, mtabembelezwa na kuwekwa magotini. Kama mama anavyoutuliza moyo wa mtoto wake, ndivyo, nami nitakavyoituliza mioyo yenu; namo Yerusalemu ndimo, mtakamotulizwa mioyo yenu. Mtakapoyaona, mioyo yenu itafurahi, nayo mifupa yenu itachipuka kama majani mabichi, nao mkono wake Bwana utajulikana kwa watumishi wake, nayo makali yake yatajulikana kwa adui zake. Kwani na mwone, Bwana anavyokuja motoni, magari yake yakikimbizwa na upepo mkali, awalipe kwa moto wa makali yake na kwa mavumo ya moto uwakao na nguvu. Kwani Bwana atawapatiliza wote wenye miili ya kimtu kwa moto na kwa upanga, nao watakaouawa naye Bwana watakuwa wengi. Wajitakasao na kujeulia matambiko ya shambani wakimfuata mtambikaji alioko kati yao, nao walao nyama za nguruwe nazo za kibudu na za panya, wote pamoja watatoweshwa; ndivyo, asemavyo Bwana. Nami ninayajua matendo yao na mawazo yao; patakuja, nitakapoyakusanya mataifa na misemo yote ya watu, nao watakuja, wauone utukufu wangu. Ndipo, nitakapowafanyizia kielekezo, nao waliookoka kwao wengine nitawatuma kwenda kwa wamizimu wa Tarsisi nako kwao wa Pulu na wa Ludu walio mafundi wa kupinda pindi, nako kwao wa Tubali na kwa Wagriki, nako kwenye visiwa vilivyoko mbali. Hawa hawajasikia habari za kwangu, hawajauona bado utukufu wangu; watautangaza utukufu wangu kwao hao wamizimu. Nao watawaleta ndugu zenu wote kuwa kipaji cha tambiko cha Bwana wakiwatoa kwenye mataifa yote; nao watapanda farasi na magari, wengine watachukuliwa katika machela, wengine watapanda nyumbu na ngamia, waje kufika Yerusalemu kwenye mlima wangu mtakatifu; ndivyo, Bwana anavyosema. Watawaleta hivyo, kama wana wa Isiraeli wanavyovipeleka vipaji vya tambiko Nyumbani mwa Bwana katika vyombo vilivyotakaswa. Namo mwao nitachukua wengine, wawe watambikaji na Walawi; ndivyo, Bwana anavyosema. Kwani kama zile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazoziumba, zitakavyokaa mbele yangu, ndivyo, mazao yenu na majina yenu yatakavyokaa; ndivyo, asemavyo Bwana. Tena itakuwa, kila mara, mwezi utakapoandama, na kila mara, siku ya mapumziko itakapokutia, wote wenye miili ya kimtu watakuja kunitambikia; ndivyo, Bwana anavyosema. Kisha watatoka mjini, waitazame mizoga ya watu walionitengua; kwani mdudu mwenye kuwaumiza hatakufa, wala moto wa kuwala hautazimika, nao watakuwa tapisho kwao wote walio wenye miili ya kimtu. Haya ni maneno ya Yeremia, mwana wa Hilkia aliyekuwa miongoni mwa watambikaji wa Anatoti katika nchi ya Benyamini. Neno la Bwana likamjia siku za Yosia, mfalme wa Yuda, mwana wa Amoni, katika mwaka wa kumi na tatu wa ufalme wake. Likamjia tena siku za Yoyakimu, mfalme wa Yuda, mwana wa Yosia, mpaka mwisho wa mwaka wa kumi na mbili wa Sedekia, mfalme wa Yuda, mwana wa Yosia, kuufikisha mwezi wa tano wa kuhamishwa kwao Wayerusalemu. Neno la Bwana likanijia kwamba: Nilipokuwa sijakutengeneza tumboni mwa mama bado, nilikujua, nawe ulipokuwa hujatoka tumboni, nilikutakasa, nikakupa kuwa mfumbuaji wa mataifa. Nami nikasema: E Bwana Mungu, tazama! Sijui kusema, kwani mimi ni kijana. Bwana akaniambia: Usiseme: Mimi ni kijana! Kwani po pote, nitakapokutuma, utakwenda; nayo yote, nitakayokuagiza, utayasema. Usiwaogope! Kwani mimi niko pamoja na wewe, nikuponye; ndivyo, asemavyo Bwana. Ndipo, Bwana alipoukunjua mkono wake, akakigusa kinywa changu, naye Bwana akaniambia: Hivi ndivyo, ninavyoyatia maneno yangu kinywani mwako. Tazama! Siku hii ya leo nimekupa kuwa mkuu wa mataifa na wa milango ya wafalme, uwe mkuu wa kung'oa na wa kuponda, wa kuangamiza na wa kubomoa, tena wa kujenga na wa kupanda. Neno la Bwana likanijia kwamba: Wewe Yeremia, unaona nini? Nikasema: Mimi ninaona tawi lenye kufunua maua. Bwana akaniambia: Umeona vema, kwani mimi nitayafumbua macho, yalilinde Neno langu, nilitimize. Neno la Bwana likanijia mara ya pili kwamba: Wewe unaona nini? Nikasema: Mimi ninaona chungu chenye maji yanayochemka, nao upande wake wa mbele ulioelekea kaskazini umegeuka. Bwana akaniambia: Upande wa kaskazini ndiko, mabaya yatakakofunuliwa, yawafikie wote wakaao nchini. Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Nitazameni! Ninaiita milango yote ya kifalme wakaao upande wa kaskazini. Nao watakuja, waweke kila mmoja wao kiti chake cha kifalme malangoni mwa Yerusalemu na ng'ambo za kuta zote za boma lake liuzungukalo, hata kwenye miji yote ya Yuda. Ndipo, nitakapowatokezea mapatilizo yangu kwa ajili ya ubaya wao wote, kwa kuwa wameniacha wakavukizia miungu mingine, wakatambikia yaliyofanywa na mikono yao. Nawe vifunge viuno vyako! Kisha inuka, kawaambie yote, nitakayokuagiza! Usizistuke nyuso zao, nisije kukustusha nyusoni pao! Tazama! Mimi nimekuweka leo kuwa ngome ya mji na nguzo ya chuma na boma la shaba, nchi zote zishindwe nao wafalme wa Yuda, nao wakuu wao, nao watambikaji wao, nao watu waliomo katika nchi hii. Watapigana na wewe, lakini hawatakuweza, kwani mimi niko pamoja na wewe. Ndivyo, asemavyo Bwana, akuponye. Neno la Bwana likanijia kwamba: Nenda kutangaza masikioni mwao Wayerusalemu kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nayakukumbukia magawio ya ujana wako na upendo wa uchumba wako, uliponifuata nyikani katika nchi isiyowezekana kupandwa mbegu. Hapo Waisiraeli walikuwa wamejitakasa kuwa wa Bwana, wakawa malimbuko ya mavuno yake; wote waliotaka kuwala wakakora manza, mabaya yakawajia; ndivyo, asemavyo Bwana. Lisikilizeni Neno la Bwana ninyi wa mlango wa Yakobo nanyi vizazi vyote vya mlango wa Isiraeli! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Baba zenu waliona mapotovu gani kwangu wakiniacha mbali wakaja kuyafuata yasiyo maana na kufanya wenyewe yasiyo maana? Hawakuuliza: Bwana yuko wapi aliyetutoa katika nchi ya Misri, aliyetuongoza nyikani katika nchi zenye jangwa na makorongo, katika nchi kavu ziuazo, katika nchi zisizopitwa na mtu, zisizokaa mtu? Nilipowapeleka katika nchi ichipukayo vizuri, myale matunda yake na mema yake, basi, hapo mlipoiingia mliitia nchi yangu machafu, iliyokuwa fungu langu mkaigeuza kuwa tapisho. Watambikaji hawakuuliza: Bwana yuko wapi? Wala wenye kazi za Maonyo hawakunijua, wabaya wakanikosea, wafumbuaji wakafumbua mambo ya Baali, wakayafuata yasiyofaa. Kwa hiyo Bwana asema: Kweli inanipasa kufuliza kuwagombeza ninyi, nao wana wa wana wenu nitawagombeza. Haya! Vukeni, mfike pwani kwa Wakiti, mwone! Tumeni watu, waje Kedari, mtambue vema na kuona, kama yamekuwako mambo kama hayo! Mwone, kama liko taifa lililoiacha miungu ya kwao na kufuata mingine, nayo siyo miungu! Nao walio ukoo wangu wameuacha utukufu wao wakifuata yasiyofaa. Yastukeni, ninyi mbingu, mambo kama hayo! Zizimukeni kwa kushangaa kabisa! ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani walio ukoo wangu wamefanya mabaya mawili: wameniacha mimi niliye kisima chenye maji ya uzima, kisha wakajichimbia visima vingine, navyo ni visima vyenye nyufa visivyoweza kushika maji. Je? Isiraeli ni mtumwa au mzalia wa nyumbani? Mbona wamekuwa mateka? Simba wanamngurumia na kupaza sauti zao, wakaigeuza nchi yake kuwa mapori tu, miji yake imeteketezwa, haina mwenye kukaa humo. Kisha Wamisri wa Nofu na wa Tahapanesi wakaulisha utosi wako. Kulikokupatia hayo siko kumwacha Bwana Mungu wako, alipotaka kukuongoza njiani? Na sasa kwa sababu gani unakwenda Misri kunywa maji ya Sihori? Tena kwa sababu gani unakwenda Asuri kunywa maji ya lile jito kubwa? Ubaya wako ndio unaokupiga, ubishi wako ndio unaokupatiliza. Yajue, yatazame, ya kuwa kumwacha Bwana Mungu wako ndiko kubaya kwenye uchungu! Nawe hukumwogopa kamwe. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu wako Mwenye vikosi. Kwani tangu kale ulivivunja vyuma vyako, ukazikata kamba zako, ukasema: Sitaki kumtumikia, ila kila kilima kirefu ulikipanda, hata kivulini kwa kila mti wenye majani mengi ukajilaza chini ukifuata ugoni. Nami ndimi, niliyekupanda, ulipokuwa tawi zuri lenyewe la mzabibu uliozaa matunda yaliyo mazuri kweli; sasa inakuwaje, ukinigeukia na kuleta machipukizi ya mzabibu mgeni? Ijapo ujioshe kwa magadi na kutumia hata sabuni nyingi, uchafu wa ubaya ulioufanya hautoki machoni pangu; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Unasemaje? Sikujichafua, sikuyafuata mambo ya Baali? Itazame njia yako ya kwenda bondeni! Yajue, uliyoyafanya huko kwa kuwa kama jike la ngamia ajiendeaye huko na huko kwa nyege zake. Ukawa kama kihongwe cha kike azoeaye nyika, naye hutwetea upepo kwa kukimbizwa na tamaa ya roho yake; tena yuko nani awezaye kuzituliza nyege zake? Lakini amtafutaye hajichokeshi: mwezi wake unapotimia, humwona upesi. Iangalie miguu yako, usivichakaze viatu! Liangalie nalo koo lako, lisipatwe na kiu! Lakini wewe hujibu: Ni kazi bure kunionya, sionyeki, kwani ninapenda wageni, nitawafuata. Kama mwizi anavyoona soni akikamatwa, vivyo hivyo nao wa mlango wa Isiraeli sharti waone soni, wafalme wao na wakuu wao na watambikaji wao na wafumbuaji wao. Maana huuambia mti: Wewe ndiwe baba yangu. Hata jiwe huliambia: Wewe ulinizaa. Lakini mimi wamenigeukia migongo, sizo nyuso; lakini siku za kupatwa na mabaya huniambia: Inuka, utuokoe! Basi, miungu yako, uliyojifanyizia, iko wapi? Na iinuke, kama inaweza kukuokoa, unapopatwa na mabaya! Kama miji yako ilivyo mingi, ndivyo, nayo miungu yako, wewe Yuda, ilivyo mingi. Mbona unanigombeza? Ninyi nyote mmenitengua; ndivyo, asemavyo Bwana. Imekuwa ya bure, nikiwapiga wana wenu, maana hawakuonyeka, panga zenu zikawala wafumbuaji wenu, kama simba wanavyoangamiza. Ninyi mlio uzao mbaya, liangalieni Neno la Bwana! Je? Nimegeuka kuwawia Waisiraeli kama nyika au kama nchi yenye giza? Kwa sababu gani walio ukoo wangu husema: Tumekwisha kujiendea, haturudi kwako tena. Je? Yuko mwanamwali asahauye kujipamba au mchumba asahauye kuvaa yapasayo ndoa? Nao walio ukoo wangu wamenisahau siku zisizohesabika. Unajuaje kuitengeneza njia yako vizuri ukitafuta wapenzi? Kweli hivyo ndivyo, ulivyojifundisha mabaya nayo katika njia zako. Kumbe hata mapindo ya nguo zako yameshikwa na damu zao wakiwa waliouawa pasipo makosa yao yo yote. Nao hukuwapata, wakipokonya, ila ni mambo yayo hayo. Kisha ukasema: Sikukosa kamwe: Kwa hiyo makali yake yameondoka kwangu. Na unione, nikikupatiliza kwa kusema kwako: Sikukosa! Mbona unatangatanga sana, uigeuze njia yako? Hata Wamisri watakutia soni, kama Waasuri walivyokutia soni. Huko nako utatoka, mikono yako ikiwa kichwani, kwani Bwana amewakataa, uliowakimbilia; kwa hiyo hakuna, utakachokipata kwao. Akasema: Kama mtu anampa mkewe ruhusa, ajiendee, naye akatoka kwake, akawa wa mume mwingine, je? Yule wa kwanza atamrudia? Nchi ile isingepata uchafu? Nawe wewe umezini na wenzio wengi, kisha unirudie mimi! ndivyo, asemavyo Bwana. Yaelekeze macho yako vilimani, utazame! Pako mahali, usipofanyiziwa ugoni? Ulikaa njiani na kuwangoja kama Mwarabu nyikani, ukaichafua nchi kwa ugoni wako uliokuwa mbaya. Kwa hiyo ulinyimwa mvua za masika, hata za vuli hazikunya, lakini paji lako ni lilelile la mwanamke mgoni, ukakataa kuingiwa na soni. Tena unaniita sasa: Baba yangu! Wewe ulikuwa mwenzangu mpendwa wa siku za ujana! Je? Atakasirika siku zote, asiniondolee makosa kale na kale? ndivyo, unavyosema; kisha unayafanya mabaya, unayoyaweza. Bwana akaniambia siku za mfalme Yosia kwamba: Umeyaona, binti Isiraeli aliyoyafanya akiniacha? Alipanda kila kilima kirefu, akakaa chini ya kila mti wenye majani mengi kufanya ugoni palepale. Alipokwisha kuyafanya hayo yote, nimesema: Rudi kwangu! Lakini hakurudi, hata dada yake binti Yuda avunjaye maagano aliyaona. Nikauona huo ugoni wote, alioufanya binti Isiraeli akiniacha, nikampa ruhusa, ajiendee, nikampa nacho cheti cha kuachana. Lakini naye dada yake binti Yuda hakuogopa, akaenda, akafanya ugoni naye. Ikawa, uvumi wa ugoni wake ukaichafua nchi, akazini akitumia mawe na miti. Alipoyafanya hayo yote, naye dada yake binti Yuda avunjaye maagano hakurudi kwangu kwa moyo wake wote, ila kwa uwongo tu; ndivyo, asemavyo Bwana. Bwana akaniambia: Binti Isiraeli akiniacha, roho yake ni njema kuliko yake binti Yuda avunjaye maagano. Nenda kuyatangaza maneno haya na kupaza sauti upande wa kaskazini, useme: Rudi, binti Isiraeli uliyeniacha! ndivyo, asemavyo Bwana: sitawatazama kwa macho makali, kwani ni mpole. Ndivyo, asemavyo Bwana; Sitakasirika kale na kale. Jua tu, ya kuwa umekora manza ulipomtengua Bwana Mungu wako ukienda huko na huko kufuata wageni chini ya kila mti wenye majani mengi, lakini sauti yangu hukuisikia; ndivyo, asemavyo Bwana. Rudini, ninyi wana mlioniacha! ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani mimi ni bwana wenu; nitawachukua mmoja katika mji mmoja, tena wawili katika udugu mmoja, niwapeleke Sioni. Nitawapa wachungaji waupendezao moyo wangu, wawachunge, mpate ujuzi wa kuerevuka. Ndivyo, asemavyo Bwana: Hapo, mtakapokuwa wengi kwa kuzaa wana katika nchi ile, siku zile hawatalitaja tena Sanduku la Agano la Bwana, halitaingia moyoni mwa mtu, hawatalikumbuka, hawatataka kuliona, wala hawatafanya jingine tena. Siku zile Yerusalemu watauita Kiti cha kifalme cha Bwana; kule Yerusalemu ndiko, wamizimu wote watakakokusanyikia kwa ajili ya Jina la Bwana, hawataendelea tena kuufuata ugumu wa mioyo yao mibaya. Siku zile mlango wa Yuda utauendea mlango wa Isiraeli, nao watakuja pamoja wakitoka katika nchi ya upande wa kaskazini, waje kuikalia nchi, niliyowapa baba zenu, iwe fungu lao. Nami nalisema: A, nitakuweka kwenye wana, nitakupa nchi ya kupendezwa nayo kwa kuwa yenye utukufu kuyapita matukufu yote ya wamizimu! Nikasema: Utaniita: Baba! Usiondoke nyuma yangu! Lakini kama mwanamke anavyomdanganya mwenziwe akimwacha, ndivyo, mlivyonidanganya na kuniacha, ninyi wa mlango wa Isiraeli; ndivyo, asemavyo Bwana. Sauti zinasikilika vilimani juu, ni kilio cha malalamiko ya wana wa Isiraeli, kwa kuwa wamezipotoa njia zao kwa kumsahau Bwana Mungu wao. Rudini, ninyi wana mlioniacha! Nitawaponya, ingawa mmeniacha. Tutazame! Tumekujia, kwani wewe ndiwe Bwana Mungu wetu. Kweli mambo ya vilimani juu ni ya uwongo tu, nayo michezo ya vileleni milimani; kweli kwake Bwana Mungu wetu ndiko, wokovu wa Isiraeli uliko. Jambo lenye soni limeyala mapato ya baba zetu tangu ujana wetu, kondoo na mbuzi wao na ng'ombe wao, hata wana wao wa kiume na wa kike. Sharti tulale kwa kupatwa na soni, nayo matusi yatufunike, kwani tumemkosea Bwana Mungu wetu, sisi na baba zetu tangu utoto wetu mpaka siku hii ya leo, hatukuisikia sauti ya Bwana Mungu wetu. Ndivyo, asemavyo Bwana: Kama utarudi, Isiraeli, rudi kwangu! Kama utayaondoa matapisho yako machoni pangu, hutafukuzwa. Ndipo, utakapoapa na kumtaja Bwana kwa kweli na kwa unyofu na kwa wongofu. Nao wamizimu watajiombea mema kwake pamoja na kumshangilia. Kwani hivyo Bwana aliwaambia waume wa Yuda nao wakaao Yerusalemu: Jilimieni shamba jipya, msipande miibani! Jitahirini, mwe wake Bwana, mkiyaondoa magovi ya mioyo yenu, ninyi waume wa Yuda nanyi mkaao Yerusalemu, kwamba: Makali yangu yasitokee yakiteketeza kama moto, watu wakishindwa kuzima, kwa ajili ya mabaya ya matendo yenu! Tangazeni katika nchi ya Yuda! Namo Yerusalemu watu na wasikie, mkisema! Pigeni baragumu katika nchi! Pazeni sauti kwa nguvu kabisa mkitangaza kwamba: Kusanyikeni, tuingie katika miji yenye maboma! Twekeni bendera, ielekee Sioni! Jihimizeni kukimbia, msisimame! Kwani mimi ninaleta mabaya kutoka upande wa kaskazini, hata mavunjiko mengi. Simba ametoka mwituni kwake kupanda kwetu, mwenye kuangamiza mataifa ameondoka, akatoka mahali pake, aigeuze nchi yako kuwa mapori, miji yako iwe mabomoko tu. Kwa hiyo jifungeni magunia! Ombolezeni na kulia! Kwani moto wa makali yake Bwana hautaondoka kwetu. Ndivyo, asemavyo Bwana: Itakuwa, siku ile moyo wa mfalme utapotea pamoja na mioyo ya wakuu wake, nao watambikaji watastuka, hata wafumbuaji watapigwa na bumbuazi. Nikasema: E Bwana Mungu! Kweli umewapoteza watu wa ukoo huu nao Wayerusalemu ulipowaambia: Mtakaa na kutengemana! Kumbe sasa upanga umewafikia rohoni! Siku zile watu wa ukoo huu nao Wayerusalemu wataambiwa: Upepo uchomao moto umetoka vilimani nyikani, ukaja kuwavumia wazaliwa wa ukoo wangu, sio wa kupunga wala wa kupepeta. Ni upepo mkali zaidi, hauiwezi kazi hiyo, ukanijia; sasa mimi nitasema nao yawapasayo, yawapate. Tazameni, anapanda kama mawingu, magari yake ni kama kimbunga, farasi wake wanakwenda mbiombio kuliko tai. A, tumekwisha kupatwa, tunaangamia. Ifueni mioyo yenu, Wayerusalemu, ubaya uitoke, mpate kuokolewa! Mawazo yako maovu yatakaa mpaka lini ndani yako? Kwani inasikilika sauti ya mtangazaji atokaye nchi ya Dani, tena mwingine anapiga mbiu ya maovu atokaye milimani kwa Efuraimu kwamba: Yakumbusheni mataifa, yaipige mbiu hii kuifikisha Yerusalemu kwamba: Wenye kuvizia wanakuja, wanatoka nchi ya mbali, waipigie miji ya Yuda makelele yao ya vita. Wanajisimamisha kama walinzi wa shamba wakiuzunguka mji, kwani umenibishia; ndivyo, asemavyo Bwana. Mwenendo wako na matendo yako yamekupatia haya; ubaya wako ndio unaokuletea huu uchungu, unakuchoma rohoni mwako. Tumboni mwangu, tumboni mwangu ndimo, ninamoona machungu, hata mwenye maganda ya moyo wangu, maana moyo wangu umenichafuka sana, siwezi kunyamaza, kwani nimesikia sauti ya baragumu rohoni mwangu na makelele ya mapigano. Inatangazwa, jinsi mavunjiko yanavyofuata mavunjiko mengine, nchi yote nzima imeharibika, mara navyo vituo vyangu vimeharibiwa pamoja na mahema yangu kwa kitambo kimoja tu. Mpaka lini nitaiona bendera? Mpaka lini nitaisikia sauti ya baragumu? Kwani walio ukoo wangu ni wapumbavu; mimi hawakunijua kwa kuwa watoto wenye ujinga wasiotambua kitu; kweli ndio wajuzi wa kufanya mabaya, lakini kufanya mema hawajui kabisa. Nilipoitazama nchi, nikaiona kuwa peke yake tu pasipo kitu cho chote; nikazitazama mbingu nazo, lakini nako hakuna mwanga. Nikaitazama milima nayo, nikaiona, inavyotukutika, hata vilima vyote vikatikisika. Nikatazama, nikaona ya kuwa hakuna mtu, hata ndege wote wa angani walikuwa wamekimbia. Nikatazama, nikaona, ya kuwa mashamba yenye matunda ni nyika, nayo miji yao yote ilikuwa imebomolewa, Bwana asiione tena kwa kuwa na makali yenye moto. Kwani Bwana alisema hivyo: Nchi yote nzima itakuwa jangwa, lakini sitaimaliza kabisa. Kwa sababu hii nchi inaomboleza, nazo mbingu huko juu zinajivika weusi; kwa sababu nimeyasema niliyoyawaza moyoni, sitajuta, wala sitarudi na kuyaacha. Kwa makelele yao wapanda farasi na wenye kuvuta pindi watu wote waliomo mijini wamekimbia, wakaingia machakani, wakapanda magengeni, miji yote ikaachwa, hakuna mtu anayekaa humo. Nawe ukiharibiwa hivyo utafanyaje? Ijapo uvae nguo nyekundu za kifalme, ujipambe mapambo ya dhahabu, hata utie wanja machoni pako, huo uzuri wako utakuwa wa bure, wapenzi wako watakubeza, tamaa zao ni kukuua tu. Nimesikia sauti kama ya mwanamke mwenye kuzaa aonaye uchungu zaidi kwa kuzaa mara ya kwanza, ni sauti ya binti Sioni, akipiga kite na kuikunjua mikono yake kwamba: A, yamenipata! Roho yangu inazimia mbele yao wauao. Tembeeni katika barabara za Yerusalemu! Tazameni, mjue! Tafuteni katika viwanja vyake, kama mnaona mtu awaye yote afanyaye yanyokayo, atafutaye welekevu! Ndipo, nitakapowaondolea makosa. Wakisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima! huapa kwa uwongo. Bwana, kumbe macho yako hayautazami welekevu? Uliwapiga, lakini hawakuzizimuka; ukawapiga tena, lakini wakakataa kuonyeka. Wakazishupaza nyuso zao kupita miamba, wakakataa kurudi. Nami nalisema moyoni: Ndio wanyonge tu walio wapumbavu hivyo, kwani hawaijui njia ya Bwana wala yampasayo Mungu wao. Na niende kwenye wakuu kusema nao! Kwani hao wanaijua njia ya Bwana nayo yampasayo Mungu wao; nikaona, hao wote pamoja wamevivunja vyuma vyao, hata kamba wamezikata. Kwa sababu hii simba wa mwituni amewapiga, naye mbwa wa jangwani akawaangamiza, naye chui huwavizia kwenye miji yao, kila atakayetoka mle araruliwe. Kwani mapotovu yao ni mengi, ukatavu wao ni wenye nguvu. Hayo nitakuachiliaje? Wanao wameniacha, huapa na kutaja isiyo miungu; nilipowashibisha, huzini, hukusanyikia nyumbani mwa wagoni. Wakatembea kama farasi walionona, kila mmoja akimlilia mke wa mwenziwe. Mambo kama hayo nisiyapatilize? ndivyo, asemavyo Bwana; watu walio hivyo roho yangu isiwalipize? Pandeni juu kutani kwao, mwaangamize! Lakini msiwamalize kabisa! Yaondoeni matawi yake! Kwani siyo yake Bwana! Kwani walio mlango wa Isiraeli nao walio mlango wa Yuda wameniacha kwa udanganyifu; ndivyo, asemavyo Bwana. Walimkana Bwana, wakasema: Hayupo, wala hakuna kibaya kitakachotujia, hatutaona upanga wala njaa. Nao wafumbuaji watakuwa upepo tu, lakini Neno halimo mwao; wenyewe na wafanyiziwe waliyoyasema. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu Mwenye vikosi anavyosema: Kwa kuwa mmesema neno hilo, mtaniona, nitayageuza maneno yangu kinywani mwako kuwa moto, nao watu wa ukoo huu watakuwa kuni, nao moto utawala. Mtaniona, ninyi wa mlango wa Isiraeli, nikiwaletea taifa litokalo mbali, ndio watu wenye nguvu, ndio watu wa kale, ndio watu, usiowajua msemo wao, usiwasikie, wakisema; ndivyo, asemavyo Bwana. Mapodo yao ni kama makaburi yaliyo wazi, wote ndio mafundi wa vita. Nao watayala mavuno yako na vilaji vyako; watawala hata wanao wa kiume na wa kike, watawala kondoo wako na ng'ombe wako, wataila mizabibu yako na mikuyu yako; wataibomoa kwa panga zao miji yako yenye maboma, uliyoikimbilia. Lakini hata siku hizo, sitawamaliza kabisa; ndivyo, asemavyo Bwana. Napo, watakapouliza: Kwa sababu gani Bwana Mungu wetu ametufanyizia hayo yote? ndipo, utakapowajibu: Kama mlivyoniacha na kutumikia miungu migeni katika nchi yenu, ndivyo, mtakavyotumikia wageni katika nchi isiyo yenu. Yatangazeni haya nyumbani mwa Yakobo, yasikilike kwa Wayuda, kwamba: Yasikieni haya, mlio watu wenye upumbavu pasipo mawazo ya moyoni! Macho mnayo, lakini hamwoni; masikio mnayo, lakini hamsikii. Mimi hamniogopi, wala uso wangu hamwuzizimukii; ndivyo, asemavyo Bwana. Nami ndimi niwekaye mchanga kuwa mpaka wa bahari, ni tengenezo la kale na kale, nayo haipapiti; ijapo ichafuke, haipashindi, ingawa mawimbi yake yaumuke, hayapapiti. Lakini wao wa ukoo huu wanayo mioyo ikataayo kutii, iliyo yenye ubishi, wakaondoka kwenda zao. Hawakusema mioyoni mwao: Na tumwogope Bwana Mungu wetu atupaye mvua za masika na za vuli, siku zao zinapotimia, atulindiaye majuma ya mavuno mwaka kwa mwaka. Lakini manza zenu zimeyatengua haya, makosa yenu yakawanyima mema. Kwani kwao walio ukoo wangu wameonekana wasionicha; wanavizia na kunyatia kama wategea ndege, hutega mitego, wakanasa watu. Kama tundu linavyojaa ndege, ndivyo, nyumba zao zinavyojaa madanganyo, kwa hiyo wakawa wakubwa, wakapata mali nyingi. Wamenenepa kwa kunona; maneno yao mabaya hupita kiasi; kuamua hawaamui, nao waliofiwa na wazazi hawawaamulii, wawaponye, wala wakiwa hawawakatii mashauri yao. Kumbe haya nisiyapatilize? Mambo kama hayo roho yangu isiyalipize? ndivyo, asemavyo Bwana. Mambo ya kustuka yazizimuayo hufanyika katika nchi hii. Wafumbuaji hufumbua yenye uwongo, nao watambikaji hufanya shauri moja nao, nao walio ukoo wangu, basi, hupenda hivyo. Lakini mtafanya nini, mwisho utakapofika? Jihimizeni kukimbia, ninyi wana wa Benyamini, mtoke Yerusalemu! Namo Tekoa pigeni baragumu! Nako kwenye Beti-Keremu twekeni bendera, kwani toka kaskazini yanakuja mabaya yanayotisha na mavunjiko yaliyo makuu. Binti Sioni aliye mzuri aliyejizoeza mororo nitamwangamiza. Watakuja kwake wachungaji na makundi yao, watapiga mahema kwake na kumzinga, walishe kila mmoja fungu lake wakisema: Jitakaseni, mpigane nao! Inukeni, tupapandie, jua lingaliko juu! A, tumechelewa sisi! Jua linataka kuchwa, vivuli vya jioni vinajivuta. Inukeni! Tupande na usiku, tuyaharibu majumba yake! Kwani ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kateni miti, kisha mwifukie kuwa boma la kuuzinga Yerusalemu! Maana ndio mji utakaopatilizwa kwa ajili ya ukorofi uliomo mwake. Kama kisima kinavyoyatoa maji yake, ndivyo, unavyoyatoa mabaya yake. Makorofi na mapotovu husikilika mwake, macho yangu huona siku zote maumivu na mapigo. Onyeka, Yerusalemu, roho yangu isije kujitenga nawe, nisikugeuze kuwa nchi yenye mapori matupu yasiyokaa watu! Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Masao yako, Isiraeli, yataokotezwa kama yake mzabibu; ukunjue tena mkono wako kama mchuma zabibu, akiyatazama matawi! Nimwambie nani na kumshuhudia, wapate kusikia? Tazama! Hawakutahiriwa penye masikio, hawawezi kusikia. Neno lake Bwana likawa kicheko kwao, hawapendezwi nalo. Nami nimejaa makali ya Bwana yenye moto, nimechoka kuyazuia. Basi, na yapige watoto wanaocheza njiani nao vijana, wakikusanyika pamoja, kwani wote, waume na wake, wazee na wakongwe, watashikwa nayo. Nyumba zao zitaachiliwa wengine, hata mashamba na wanawake vilevile, kwani nitawakunjulia mkono wangu wao wakaao katika nchi hii; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani wao wote, walivyo wadogo mpaka wakiwa wakubwa, hutamani mali tu; hata wafumbuaji na watambikaji wote pia hufanya yenye uwongo. Madonda yao walio wazaliwa wa ukoo wangu huyaponya juujuu wakisema: Tengemaneni! Tengemaneni! lakini hakuna utengemano. Watapatwa na soni, kwani hufanya yatapishayo; lakini hawaoni soni, wala hawajui kuiva nyuso. Kwa hiyo wataanguka pamoja na wenzao watakaoanguka siku hiyo, nitakapowapatiliza; ndipo, watakapojikwaa. Ndivyo, Bwana anavyosema. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Simameni njiani, mwone! Ulizeni mapito ya kale, kama njia njema ni ipi? Hiyo ishikeni, mzipatie roho zenu kituo! Wakasema: Hatutaishika. Nitawawekea walinzi, mwiangalie sauti ya baragumu! Wakasema: Hatutaiangalia. Kwa hiyo sikieni, ninyi wamizimu! Ninyi mliokutanika, yatambueni yatakayokuwa kwao! Nayo nchi, sikia! Na mnione, nikiwaletea mabaya watu wa ukoo huu, ndiyo yaliyozaliwa na mawazo yao, kwani maneno yangu hawakuyasikiliza, nayo Maonyo yangu wameyakataa. Uvumba utokao Saba unanifaliaje? Nayo manukato yatokayo nchi ya mbali ni ya nini? Ng'ombe zenu za tambiko hazinipendezi, wala vipaji vyenu vya tambiko havinifurahishi. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nitazameni, jinsi ninavyoweka mawe ya kukwazia njiani kwao walio ukoo huu, nao watajikwaa wote pia, baba na watoto, wenyeji na wenzao wataangamia. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazameni! Watu watakuja toka nchi ya kaskazini, taifa kubwa litainuka kwenye mapeo ya nchi. Hushika pindi na mikuki, ni wakorofi pasipo huruma, makelele yao ni kama kuvuma kwa bahari, nao hupanda farasi; wamejivika kama watu waendao vitani, wapigane na wewe, binti Sioni. Tulipokisikia kivumo chao, mikono yetu ikalegea, tukasongeka, uchungu ukatushika kama wa mzazi. Msitoke kwenda shambani, wala njiani msiende! Kwani panga za adui ziko, zinawastusha po pote. Mlio wazaliwa wa ukoo wangu, jivikeni magunia, mpate kugaagaa mavumbini! Ombolezeni kama waliofiwa na mwana wa pekee! Vilio na viwe vyenye uchungu sana! Kwani mara mwangamizi atatujia. Nimekuweka kwao walio ukoo wangu, uwajaribu, kwani ni wagumu, uwatambue ukizijaribu njia zao. Wao wote ndio wabishi wenyewe waendao wakisingizia, ni wagumu kama shaba na vyuma, wao wote ndio wapotezaji wabaya. Mifuo ikifukutwa, mle motoni hutoka shaba tu. Imekuwa kazi bure kuyeyusha mara kwa mara, kwani mabaya yaliyomo hayakutengeka. Sharti waitwe fedha zitupwazo, kwani Bwana amewatupa. *Neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana ni hili: Simama langoni mwa Nyumba ya Bwana, ulitangaze neno hili huko ukisema: Lisikieni neno la Bwana, ninyi Wayuda wote mnaoingia humu malangoni kumwangukia Bwana! Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli: Ziangalieni njia zenu na matendo yenu, yawe mema! Ndipo, nitakapowakalisha katika nchi hii. Msijiegemeze maneno ya uwongo kwamba: Nyumba ya Bwana, Nyumba ya Bwana, Nyumba ya Bwana ni hii! Ila jikazeni, njia zenu na matendo yenu yawe mema, mfanyiziane yanyokayo kila mtu na mwenziwe! Msiwakorofishe wageni wala wafiwao na wazazi wala wajane! Wala msimwage mahali hapa damu zao wasiokosa! Wala msifuate miungu mingine! Maana hivyo mnajipatia mabaya. Ndipo, nitakapowakalisha mahali hapa katika nchi hii, niliyowapa baba zenu, iwe yao tangu kale hata kale. Tazameni! Ninyi mnaojiegemeza maneno ya uwongo yasiyofaa: Huiba, huua, huzini, huapa kwa uwongo, humvukizia Baali, hufuata miungu mingine, msiyoijua. Kisha mnakuja kusimama machoni pangu katika Nyumba hii iliyoitwa kwa Jina langu, mkasema: Tumepona! mpate kuyafanya matapisho hayo yote. Je? Nyumba hii iliyoitwa kwa Jina langu imegeuka kuwa pango la wanyang'anyi machoni penu? Mimi nami ninayaona kweli. Ndivyo, asemavyo Bwana.* Haya! Nendeni mahali pangu kule Silo, nilipolikalisha Jina langu kwanza, myaone yote, niliyopafanyizia kwa ajili ya ubaya wao Waisiraeli walio ukoo wangu! Sasa ndivyo, asemavyo Bwana: nanyi mmeyafanya hayo matendo yote, tena nalisema nanyi pasipo kuchoka kusema, lakini hamkusikia, nikawaita, lakini hamkuitikia. Kwa hiyo nitaifanyizia Nyumba hii iliyoitwa kwa Jina langu, ninyi mnayoitumia ya kujiegemezea, hata mahali hapo, nilipowapa ninyi na baba zenu, nitapafanyizia, kama nilivyofanya huko Silo. Nitawatupa, mwondoke machoni pangu, kama nilivyowatupa ndugu zenu wote pia walio kizazi chake Efuraimu. Wewe nawe usiwaombee wao wa ukoo huu! Wala usipaze sauti kunilalamikia kwa ajili yao, wala usinihimize! Kwani hapo sikusikii. Huyaoni, wanayoyafanya katika miji ya Yuda namo Yerusalemu katika barabara zake? Watoto huokota kuni, nao baba huziwasha moto, wanawake wakikanda unga wa kufanya vikate vya mfalme wa kike wa mbinguni, tena humwaga vinywaji vya kutambikia miungu mingine, kusudi waniumize moyoni. Ndivyo, asemavyo Bwana: Hao watakao kuniumiza mimi hawajiumizi wenyewe, nyuso zao zipate kutiwa soni? Kwa hiyo hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wataona, jinsi makali yangu yenye moto yatakavyomwagwa mahali hapa, yachome watu na nyama na miti ya mashamba na mazao ya nchi, yawake moto usiozimika. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Ng'ombe zenu za tambiko za kuteketezwa nzima ziongezeni kwa ng'ombe zenu za tambiko za kuchinjwa, mpate kula nyama. Kwani sikuwaambia baba zenu, wala sikuwaagiza, nilipowatoa katika nchi ya Misri, watoe ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kuchinjwa. Kweli niliwaagiza neno hili tu kwamba: Isikieni sauti yangu! Ndivyo, nitakavyokuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa ukoo wangu. Kisha zishikeni njia zote, nitakazowaagiza, mpate kuona mema! Lakini hawakusikia, wala hawakuyatega masikio yao, wakaendelea kwa mashauri na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakanionyesha migongo, lakini sizo nyuso. Vikawa hivyo tangu siku ile, baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri mpaka siku hii ya leo; nami nalituma kwenu watumishi wangu wote walio wafumbuaji, sikuchoka hata siku moja. Lakini hawakunisikia, wala hawakuyatega masikio yao, wakazishupaza kosi zao, wakafanya mabaya kuwashinda baba zao. Nawe ukiwaambia maneno haya yote, hawatakusikia, ukiwaita, hawatakuitikia. Basi, uwaambie: Taifa hili ndilo lisiloisikia sauti ya Bwana Mungu wao, wala hawakutaka kuonyeka. Welekevu umepotea, umetoweka vinywani mwao. Binti Sioni, zinyoe nywele zako za urembo, uzitupe! Piga kilio vilimani juu kusikokuwa na vijiti! Kwani Bwana amekikataa kizazi kilichomkasirisha, akakitupa. Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Wana wa Yuda wamefanya yaliyo mabaya machoni pangu, wakaweka matapisho yao katika Nyumba hii inayoitwa kwa Jina langu, waichafue. Wakapajenga pa kumtambikia Tofeti katika bonde la Mwana wa Hinomu, wateketeze hapo motoni wana wao wa kiume na wa kike; nami sikuwaagiza hivyo, wala havikunijia moyoni. Kwa hiyo ndivyo, asemavyo Bwana: Wataona kweli, siku zikija, pasipotajwa tena Tofeti wala bonde la Mwana wa Hinomu, ila pataitwa Bonde la Uuaji; ndipo, watakapozikia kwenye Tofeti kwa kukosa pengine. Nayo mizoga ya watu wa ukoo huu itakuwa chakula cha ndege wa angani na cha nyama wa porini, asiweko atakayewatisha. Ndipo, nitakapokomesha katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu sauti za vicheko na sauti za furaha, hata sauti za wachumba wa kiume na wa kike, kwani nchi hii itakuwa mavunjiko tu. Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku zile wataifukua makaburini mwao mifupa ya wafalme wa Yuda na mifupa ya wakuu wao na mifupa ya watambikaji na mifupa ya wafumbuaji na mifupa yao waliokaa Yerusalemu. Kisha wataitandaza penye jua na penye mwezi napo penye kikosi chote cha mbinguni, maana wamepapenda, wakapatunukia, wakapafuata, wakapatafuta, wakapaangukia; haitaokotwa, wala haitazikwa tena, itakuwa mbolea tu juu ya nchi. Nayo masazo yote yatakayosazwa ya mlango huu mbaya yatapendezwa zaidi na kufa kuliko kuwapo mahali po pote, nilipowatupia hayo masazo; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. *Uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Je? Wako waangukao wasioinuka tena? Au yuko ageukaye asiyerudi tena? Mbona ukoo huu wa Yerusalemu umegeuka pasipo kurudi kale na kale? Wameyashika madanganyifu, wakakataa kurudi. Nikaangalia na kusikiliza, hawasemi yaliyo sawa, wala hakuna mtu aujutiaye ubaya wake kwamba: Je? Nimefanya nini? Kila mmoja hugeuka kwa kujikimbilia kwao kama farasi akimbiaye vitani. Naye korongo wa angani huzijua siku zake, hata hua na kinega na mbayuwayu huzishika siku zao za kuja, lakini walio ukoo wangu hawayajui yampasayo Bwana. Mnasemaje: Sisi tu werevu wa kweli, nayo Maonyo yake Bwana tunayo? Ndio, lakini tazameni! Kalamu zao waandishi zenye uwongo zimeyageuza kuwa uwongo! Walio werevu wa kweli wamepatwa na soni, wanazizimuka kwa kuumbuliwa; Neno lake Bwana wamelitupa, sasa wako na werevu gani tena ulio wa kweli?* Kwa hiyo nitawapa wengine wake zao, nayo mashamba yao nitawapa wale watakaowatwaa, kwani wao wote, walivyo wadogo mpaka wakiwa wakubwa, hutamani mali tu, hata wafumbuaji na watambikaji wote pia hufanya yenye uwongo. Madonda yao walio wazaliwa wa ukoo wangu huyaponya juujuu wakisema: Tengemaneni! Tengemaneni! Lakini hakuna utengemano. Watapatwa na soni, kwani hufanya yatapishayo; lakini hawaoni soni, wala hawajui kuiva nyuso. Kwa hiyo wataanguka pamoja na wenzao watakaoanguka siku hiyo, nitakapowapatiliza; ndipo, watakapojikwaa; ndivyo, Bwana anavyosema. Ndivyo, asemavyo Bwana: Ninapotaka kuchuma kwao, mizabibu, haina zabibu, wala mikuyu haina kuyu, nayo majani yao inakuwa inanyauka; kwa hiyo nitatoa watu, wawaondoe. Mbona sisi tunajikalia? Na tukusanyike, tuingie katika miji yenye maboma, tukaangamie humo! Kwani Bwana Mungu wetu atatuangamiza na kutunywesha maji yenye sumu, kwa kuwa tumemkosea Bwana. Mbona tunangojea utengemano? Lakini hakuna chema! Mbona tunangojea siku za kupona? Lakini tunayoyaona ni mastuko. Upande wa Dani kunasikilika, farasi wao wanavyofoka, kwa uvumi wa makelele yao walio wenye nguvu nchi hii yote inatetemeka; watakuja, wataila nchi nayo yote yaliyomo, miji pamoja nao wakaaamo. Angalieni! Nitatuma kwenu nyoka za pili wasiowezekana kwa uganga wo wote, wawaume ninyi; ndivyo, asemavyo Bwana. Napata wapi utulivu wa roho katika masikitiko? Moyo wangu umeugua humu ndani. Nikiangalia ninasikia sauti za vilio vyao walio wazaliwa wa ukoo wangu, zikitoka katika nchi ya mbali kwamba: Je? Bwana hayumo naye? Sioni wala mfalme wake hayumo naye? Kwa sababu gani wamenisikitisha na vinyago vyao na mambo mageni yasiyo maana? Mavuno yamepita, kiangazi kimekwisha, lakini sisi hatukuokolewa. Kwa mavunjiko yao walio wazaliwa wa ukoo wangu nami nimevunjika, nikaomboleza, ushangao ukanishika kwa nguvu. Je? Haiko miti yenye dawa huko Gileadi? Wala hakuna mponya huko? Mbona wazaliwa wa ukoo wangu hawakupata kuponywa? Nataka sana, kichwa changu kingegeuka kuwa maji, nayo macho yangu yangegeuka kuwa kisima cha machozi, nipate kuwalilia mchana na usiku wazaliwa wa ukoo wangu waliouawa! Nataka sana, ningepata nyikani fikio la wasafiri, ningewaacha wao walio ukoo wangu na kutoka kwao, kwani wao wote ndio wagoni, ni chama cha wadanganyi. Huzikaza ndimi zao kuwa pindi za kupiga maneno ya uwongo; wamepata nguvu katika nchi, lakini si kwa welekevu, kwani wakitoka pabaya huingia pabaya pengine, lakini mimi hawanijui; ndivyo, asemavyo Bwana. Jilindeni kila mtu kwa ajili ya mwenziwe! Hata ndugu na ndugu msiegemeane! Kwani kila ndugu humponza ndugu yake, hata kila rafiki hufuata masingizio. Kila mmoja humwongopea mwenziwe, lakini neno la kweli hawalisemi, wakazifunza ndimi zao kusema uwongo, hupotoa, mpaka wachoke. Unakaa kwenye madanganyifu katikati, nami kwa udanganyifu wamekataa kunijua; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwa hiyo Bwana Mwenye vikosi anasema hivi: Kweli wataniona, nikiwayeyusha na kuwajaribu. Kwani nifanye mengine gani nikiwatazama wazaliwa wa ukoo wangu? Ndimi zao ni mishale ya kuchoma na kuua, husema madanganyifu: kwa vinywa vyao husema matengemano na wenzao, lakini mioyoni huviziana. Mambo kama hayo nisiyapatilize kwao? watu walio hivyo Roho yangu isiwalipize? ndivyo, asemavyo Bwana. Milima nitaililia na kuiombolezea, nazo mbuga za nyikani nitazitungia wimbo wa kilio, kwani ziko peke yao, hakuna mtu apitaye hapo, hapasikiliki tena sauti za ng'ombe, hata ndege wa angani pamoja na nyama wa porini wamekimbia kwenda zao. Hata Yerusalemu nitaugeuza kuwa machungu ya mawe tu, panapokaa mbwa wa mwitu, nayo miji ya Yuda nitaigeuza kuwa peke yao, isikae watu. Yuko nani aliye mwerevu wa kweli, ayatambue haya? Yuko nani, ambaye kinywa cha Bwana kilisema naye, ayatangaze, kama ni kwa sababu gani, nchi hii ikiangamia, iwe peke yake, pasipite mtu? Bwana akasema: Kwa sababu wameyaacha Maonyo yangu, niliyowapa, wayaangalie, wakakataa kuisikia sauti yangu, hawakuifuata. Ila wameufuata ushupavu wa mioyo yao, wakayafuata Mabaali, kama baba zao walivyowafundisha. Kwa hiyo Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anasema hivi: Wataniona kweli, nikiwalisha majani machungu na kuwanywesha maji yenye sumu. Nitawatawanya kwenye wamizimu, wasiowajua hawa wala baba zao, tena nitatuma panga nyuma yao, mpaka niwamalize. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Yatambueni! Waiteni wanawake waombolezaji, waje! Tumeni nako kwao wanawake walio werevu wa kweli, waje! Waje upesi kutuombolezea, macho yetu yachuruzike machozi, nazo kope zetu zitiririke maji! Sauti za maombolezo zinasikilika upande wa Sioni kwamba: Tumetekwa namna gani na kutwezwa kabisa? Hatuna budi kuiacha nchi yetu, kwani makao yetu wameyabwaga chini. Sasa ninyi wanawake, lisikieni neno la Bwana, masikio yenu yalipokee neno la kinywa chake! Wafundisheni wana wenu wa kike kuomboleza, kila mwanamke mmoja amfundishe mwenziwe kulilia kufa kwamba: Kifo kimepanda madirishani mwetu, kimeingia majumbani mwetu, kiwapokonye watoto barabarani mwa mji, nao wavulana viwanjani! Sema: Ndivyo, asemavyo Bwana: Mizoga ya watu itaanguka shambani kuwa kama vinyesi au kama miganda inavyoanguka chini nyuma ya mvunaji, lakini hakuna mwenye kuiokota. *Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mwerevu wa kweli asijivunie werevu wake! Wala mwenye nguvu asijivunie nguvu zake! Wala mwenye mali asijivunie mali zake! Ila mwenye kujivuna na ajivunie kuwa mtambuzi wa kunijua mimi, ya kuwa mimi Bwana ndiye afanyaye upole na maamuzi yaongokayo katika nchi hii! Kwani hayo ndiyo yanipendezayo; ndivyo, asemavyo Bwana.* Ndivyo, asemavyo Bwana: Tazameni! Siku zinakuja, nitakapowapatiliza wote waliotahiriwa kwa kuwa tena kama watu wasiotahiriwa, akina Wamisri na Wayuda na Waedomu nao wana wa Amoni na Wamoabu nao wote wakatao nywele za panjani wakaao nyikani; kwani wamizimu wote ni watu wasiotahiriwa miilini, lakini wote walio wa mlango wa Isiraeli ni wenye mioyo isiyotahiriwa. Lisikieni neno, Bwana alilowaambia ninyi wa mlango wa Isiraeli! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msijifundishe kuzishika njia za wamizimu! Wala vielekezo vya mbinguni msivistuke, kwa kuwa wamizimu wanavistuka! Kwani miiko ya watu wa kimizimu ni kitu pasipo maana; kwani hukata mti wa mwituni, mikono ya fundi ikautengeneza kwa tezo. Kisha huupamba kwa fedha na kwa dhahabu, akautia nguvu kwa misumari na nyundo, usitukutike. Huwa kama nguzo tu iliyofunikizwa, hausemi; sharti uchukuliwe, kwani hauendi. Msiiogope! Kwani haifanyi kibaya, wala haina nguvu ya kutupatia mema. Hakuna afananaye na wewe, Bwana! Mkuu ndiwe wewe, nalo Jina lako ni kuu lenye nguvu. Yuko nani asiyepaswa na kukuogopa, uliye mfalme wa wamizimu? Inakupasa kweli, uogopwe; kwani miongoni mwa werevu wote wa kimizimu, hata katika nchi za kifalme zote hakuna afananaye na wewe. Wote pamoja ni wajinga na wapumbavu, mafundisho yao wasio kitu ndiyo mti mtupu! Mabati ya fedha yaliyopigwa nyundo huletwa toka Tarsisi, nayo ya dhahabu hutoka Ufazi, mafundi huyatengeneza, kisha mikono ya wafua dhahabu huyaseneza. Mavazi yao ni nguo za kifalme, nyeusi na nyekundu. Yote pia ni kazi za mafundi wazijuao kazi zao. Lakini Bwana ndiye Mungu kweli, yeye ni Mungu Mwenye uzima na mfalme wa kale na kale. Ukali wake huitetemesha nchi, wamizimu hawawezi kuyavumilia machafuko yake. Kwa hiyo mtawaambia: Miungu isiyoziumba mbingu na nchi sharti iangamie ulimwenguni chini ya mbingu. Yeye ndiye aliyeifanya nchi kwa uwezo wake, akausimika ulimwengu kwa werevu wake wa kweli, akazitanda mbingu kwa utambuzi wake. Huvumisha maji mbinguni kwa ngurumo na kupandisha mawingu yatokayo mapeoni kwa nchi, kisha hupiga umeme kwenye mvua na kutoa upepo huko, alikouweka. Ndipo, kila mtu anapopumbaa tu, asijue yatokako, hata kila mfua dhahabu hupatwa na soni kwa ajili ya kinyago chake, kwani alichokitengeneza ni uwongo tu, hata pumzi haimo. Havina maana, ni kazi ya kuchekwa tu; siku vitakapopatilizwa huangamia. Lakini aliye fungu lake Yakobo hafanani navyo, kwani yeye ndiye aliyeyatengeneza yote, naye Isiraeli ni ukoo uliopata fungu kwake; Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake. Yakusanye yaliyo yako katika nchi hii, wewe ukaaye bomani bado! Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona mara hii, nikiwatupa kwa nguvu wakaao katika nchi hii, nitawasonga, wapate kuona! A, nimevunjika! Pigo langu halitapona! Nasema mwenyewe: Haya ndiyo manyonge yangu, sharti niyavumilie. Hema langu limeharibika, nazo kamba zangu zote zimekatika; watoto wangu wametoka kwangu, hawako; hakuna atakayelipiga hema langu tena na kuziwamba nguo zangu za hema. Kwani wachungaji wangu wamepumbaa, hawakumtafuta Bwana, kwa hiyo hawakuerevuka, nalo kundi lao lote likatawanyika. Sikilizeni! Sauti zinasikilika zinazokuja, ni uvumi mkubwa sana upande wa kaskazini! Wanataka kuigeuza miji ya Yuda kuwa mapori tu na makao ya mbwa wa mwitu. Ninajua, Bwana, ya kuwa mtu siye anayeilinganya njia yake, wala mtu aendaye siye anayeushupaza mwenendo wake. Nipige, Bwana, mapigo yapasayo! Usinipige kwa ukali wako, usiniangamize! Makali yako yenye moto yamwage penye wamizimu wasiokujua, napo penye koo za watu wasiolitambikia Jina lako! Kwani wamemla Yakobo, kweli wamemla na kummaliza, nayo makao yake wameyageuza kuwa mapori tu. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwake Bwana kwamba: Yasikieni maneno ya agano hili, myaambie watu wa Yuda nao wakaao Yerusalemu! Utawaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Ameapizwa kila asiyeyasikia maneno ya agano hili, niliyowaagiza baba zenu siku ile, nilipowatoa katika nchi ya Misri katika tanuru ya kuyeyushia vyuma kwamba: Isikilizeni sauti yangu, myafanyize yote, nitakayowaagiza! Ndivyo, mtakavyokuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wenu, kusudi nikitimilize kiapo, ambacho niliwaapia baba zenu cha kwamba: Nitawapa nchi ichuruzikayo maziwa na asali, kama ilivyo na siku hii ya leo. Ndipo, nilipojibu nikisema: Amin, Bwana. Bwana akaniambia: Yatangaze maneno haya yote katika miji ya Yuda namo barabarani mwa Yerusalemu kwamba: Yasikilizeni maneno ya agano hili, myafanyize! Kwani nimeyashuhudia baba zenu siku ile, nilipowatoa katika nchi ya Misri, mpaka siku hii ya leo sikuchoka kuwashuhudia na kuwahimiza kwamba: Isikieni sauti yangu! Lakini hawakuisikia, wala hawakuyatega masikio yao, wakaendelea kila mmoja kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, kwa hiyo nikawatimizia maneno yote ya hilo agano, nililowaagiza, walifanye, lakini hawakulifanya. Bwana akaniambia: Yameonekana mapatano mabaya ya watu wa Yuda nao wakaao Yerusalemu: wameyarudia mabaya ya baba zao wa kale walikataa kuyasikiliza maneno yangu, wakafuata miungu mingine, waitumikie. Walio mlango wa Isiraeli nao walio mlango wa Yuda wamelivunja agano langu, nililolifanya na baba zao. Kwa hiyo Bwana anasema hivi: Kweli wataniona, nikiwaletea mabaya, wasiyoweza kuyatoka. Ndipo, watakaponililia, lakini sitawasikia. Kisha miji ya Yuda nao wakaao Yerusalemu watakwenda kuililia miungu, waliyoivukizia, lakini haitawaokoa siku za kupatwa na mabaya. Kwani kama miji yako ilivyo mingi, ndivyo, miungu yako, Yuda, ilivyo mingi nayo. Tena kama barabara za Yerusalemu zilivyo nyingi, ndivyo, palivyo pengi napo, mlipopatengeneza pa kuitambikia iliyo yenye soni, ndipo pa kumvukizia Baali. Wewe nawe usiwaombee wao wa ukoo huu! Wala usipaze sauti kunilalamikia kwa ajili yao! Kwani mimi sisikii, wanaponiita, kwa ajili ya ubaya wao. Waliokuwa wapenzi wangu wanataka nini Nyumbani mwangu? Mkiyafanya mawazo yenu mabaya yaliyo mengi, nyama takatifu zitayaondoa, yawatoke ninyi? Nanyi mnapofanya mabaya, ndipo, mnapofurahi. Bwana alikuita jina lako mchekele wenye majani mengi wa kupendeza macho kwa kuzaa vizuri, lakini sasa wengi wanaupigia makelele makubwa, maana ameuwashia moto wa kuuchoma, nayo matawi yake yamevunjika. Kwani Bwana Mwenye vikosi aliyekupanda amesema mabaya yatakayokujia kwa ajili ya mabaya, wao wa mlango wa Isiraeli nao wa mlango wa Yuda waliyonifanyizia, wanikasirishe, wakimvukizia Baali. Bwana akanijulisha, ndipo, nilipojua, kisha akanionyesha matendo yao. Mimi nikawa kama mwana kondoo mwanana anayepelekwa kuchinjwa, sikujua, ya kama walikuwa wameniwazia mimi mawazo ya kwamba: Na tuuangamize mti na matunda yake! Na tuung'oe katika nchi yao walio hai, jina lake lisikumbukwe tena! Lakini wewe Bwana Mwenye vikosi, unakata mashauri yaongokayo, unajaribu mafigo na mioyo; na nione, jinsi unavyowalipiza, kwani nimekusukumia wewe shauri langu. Kwa hiyo Bwana anasema hivyo kwa ajili ya watu wa Anatoti walioitafuta roho yako wakisema: Usitufumbulie kwa Jina la Bwana, usiuawe na mikono yetu! Kwa hiyo Bwana Mwenye vikosi anasema hivi: Utaniona, nikiwapatiliza: vijana wao watakufa kwa panga, nao watoto wao wa kiume na wa kike watakufa kwa njaa. Lakini masao hayatakuwako, kwani watu wa Anatoti nitawaletea mabaya mwaka ule, watakapopatilizwa. Wewe Bwana hushinda, nikiulizana wa wewe; lakini na tusemeane hukumu zipasazo! Mbona njia zao wasiokucha huendelea vema, nao wadanganyifu wanaodanganya hutengemana? Uliwapanda, wakatia mizizi; huendelea kukua, mpaka wakizaa matunda. Wewe u karibu vinywani mwao, lakini u mbali mioyoni mwao. Nawe Bwana unanijua, ukaniona, ukanijaribu moyo wangu, kama u kwako. Wakamate kama kondoo wa kuchinjwa, kawachagulie, wawe tayari siku ya kuchinjwa! Nchi na iomboleze mpaka lini, majani ya mashamba yote yakinyauka? Kwa ajili ya ubaya wao waikaao hata nyama na ndege wametoweka, nao husema: Hatauona mwisho wetu! Kama waendao kwa miguu wamekuchokesha, ulipokimbizana nao, utawezaje kushindana na farasi? Tena: Wewe ukitulia tu katika nchi itengemanayo utafanyaje ukikaa katika machaka makuu ya Yordani? Kwani nao ndugu zako nao mlango wa baba yako hukudanganya, kweli hawa nao hupaza sauti za kupiga kelele nyuma yako; usiwategemee! Kwani usoni pako husema mema. Nimeiacha Nyumba yangu, nikalitupa fungu langu, nikayatoa, roho yangu iliyopendezwa nayo, nikayatia mikononi mwa adui zao. Fungu langu likaniwia kama simba wa mwituni: Ameningurumia, kwa hiyo nimechukiwa naye. Je? Fungu langu ni kama bundi, ambaye makunguru humkusanyikia po pote? Nendeni kuwakusanya nyama wote wa porini! Kisha waleteni, wale! Wachungaji wengi wameiharibu mizabibu yangu, wakalikanyagakanyaga fungu langu; fungu langu, nililopendezwa nalo sana, wameligeuza kuwa mapori kama ya nyikani. Kweli wameligeuza kuwa peke yake tu; hivyo lilivyo peke yake linanililia, nchi hii nzima iko peke yake, kwa kuwa hakuwako mtu aliyeyaweka hayo moyoni. Milimani po pote katika nyika wenye kuiharibu nchi wamefika; kwani Bwana yuko na upanga ulao; huanzia kula kwenye mpaka mmoja wa nchi, hata ufike kwenye mpaka mwingine. Ndipo, wote wenye miili wanapokosa kutengemana. Walipopanda ngano huvuna miiba; hujisumbua, lakini hawapati kitu. Ndivyo, mtakavyopatwa na soni kwa ajili ya mavuno yenu, moto wa makali yake Bwana utakapowaka. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya wabaya wote, tuliokaa nao, waliolitwaa fungu lile, nililowapa wao walio ukoo wangu wa Isiraeli, liwe fungu lao: Wataniona, nikiwang'oa katika nchi yao, tena nikiwang'oa walio wa mlango wa Yuda katikati yao! Itakuwa, nitakapokwisha kuwang'oa nitawahurumia tena, niwarudishe kila mmoja penye fungu lake, kila mmoja katika nchi yake. Tena itakuwa, kama wale watajifundisha vema njia zao walio ukoo wangu, waape na kulitaja Jina langu na kusema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, kama wenyewe walivyowafundisha walio ukoo wangu kuapa na kumtaja Baali, basi, ndipo, watakapojengwa katikati yao walio ukoo wangu. Lakini kama hawasikii, nitaling'oa taifa hilo kabisa, liangamie; ndivyo, asemavyo Bwana. Hivi ndivyo, Bwana alivyoniambia: Nenda kujinunulia mshipi wa amerekani, ujifunge viunoni! Lakini usiutie majini! Nikaununua mshipi, kama Bwana alivyoniagiza, nikajifunga viunoni. Neno la Bwana likanijia mara ya pili kwamba: Uchukue mshipi, ulioununua, ulio viunoni pako! Kisha inuka, uende kwenye Furati, uufiche kule katika ufa wa mwamba! Nikaenda, nikauficha kule Furati, kama Bwana alivyoniagiza. Ikawa, siku nyingi zilipopita, ndipo, Bwana aliponiambia: Inuka, uende Furati, uuchukue kule mshipi, niliokuagiza kuuficha huko. Nikaenda Furati, nikauchimbua, nikauchukua ule mshipi mahali hapo, nilipouficha; lakini nilipoutazama ule mshipi, ulikuwa umeharibika, haukufaa kitu cho chote. Ndipo, neno la Bwana liliponijia kwamba: Bwana anasema hivi: Hivi ndivyo, nitakavyoyaharibu majivuno ya Yuda nayo majivuno ya Yerusalemu yaliyo mengi. Watu wa ukoo huu mbaya wamekataa kuyasikia maneno yangu, wakajiendea kwa ushupavu wa mioyo yao, wakafuata miungu mingine wakiitambikia na kuiangukia; basi, watakuwa kama mshipi huu usiofaa kitu cho chote. Kwani kama mshipi unavyoambatana na viuno vya mtu, ndivyo, nilivyowaambatanisha na mimi wote walio wa mlango wa Isiraeli nao wote walio wa mlango wa Yuda, wawe ukoo wangu wa kulikuza Jina langu, wakilishangilia na kulitukuza, lakini hawakusikia; ndivyo, asemavyo Bwana. Basi, utawaambia neno hili: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Viriba vyote na vijazwe mvinyo! Wakikuuliza: Hatujui, ya kuwa viriba vyote hujazwa mvinyo? ndipo, utakapowaambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikiwajaza ulevi wote wakaao katika nchi hii, wafalme wanaokikalia kiti cha kifalme cha Dawidi na watambikaji na wafumbuaji nao wote wakaao Yerusalemu. Kisha nitawaponda kila mtu kwa ndugu yake, hata wababa na wana pamoja, sitawaonea uchungu, wala sitawachagulia, wala sitawahurumia, nisiwaangamize; ndivyo, asemavyo Bwana. Sikieni na kusikiliza vema! Msijikweze! Kwani Bwana anasema: Mtukuzeni Bwana Mungu wenu, akingali hajaleta giza bado, mkingali hamjajikwaa miguu yenu milimani penye giza! Maana mtangoja, pawe mwanga, naye ataugeuza kuwa kivuli kiuacho akiufunikiza mawingu meusi. Lakini msiposikia, roho yangu itayalilia majivuno yenu mafichoni, nayo macho yangu yatachuruzika machozi pasipo kukoma, kwa kuwa kundi la Bwana limetekwa. Mwambie mfalme na mama yake: Jinyenyekezeni, mkae chini! Kwani vichwani penu vilemba vya urembo vimeanguka chini! Miji ya upande wa kusini imefungwa, tena hakuna anayeifungua, Wayuda wote wametekwa, kweli wote pia wametekwa. Yainueni macho yenu, mwaone wanaokuja toka kaskazini! Kundi ulilopewa liko wapi, wale kondoo wako wenye utukufu? Utasemaje, akikuwekea wale kuwa wakuu wako, uliowazoeza kuwa rafiki zako wapendwa? Wao watakapokuwa wakuu, hautakushika uchungu kama wa mwanamke anayetaka kuzaa? Kama unauliza moyoni mwako: Mbona haya yamenitukia? ujue: Kwa mabaya yako mengi, uliyoyafanya, nguo zako zenye mapindo marefu zimefunuliwa, hata miguu yako ikatokezwa nje kwa kukorofishwa hivyo. Je? Mtu mweusi anaweza kuigeuza ngozi yake? Au chui anaweza kuyaondoa madoadoa yake? Kama ndivyo, mngeweza kufanya mema nanyi mliofundishwa kufanya mabaya. Kwa hiyo nitawatawanya kama makapi yapeperushwayo na upepo wa nyikani. Haya ndiyo, uliyopatiwa na kura, ni fungu lako, ulilopimiwa na mimi, kwa kuwa umenisahau, ukaegemea mambo ya uwongo; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwa hiyo mimi nami nitazipandisha nguo zako zenye mapindo marefu na kuziweka usoni pako, yako yenye soni yaoneke. Uzinzi wako na vilio vyako vya utongozi na uovu wako wa kuziwaza njia za ugoni za kwenda vilimani au mashambani, nimeyaona hayo matapisho yako. Yatakupata, wewe Yerusalemu, usieuliwe! Yatakuwa hivyo mpaka lini? Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Yeremia kwa ajili ya kupotea kwa mvua: Yuda huomboleza, nao waliomo malangoni mwake wamefifia kwa kukaa mchangani na kuvaa nguo nyeusi, navyo vilio vya Yerusalemu hupanda juu. Wakuu wao huwatuma walio wadogo kwao kwenda majini; lakini wakifika visimani hawaoni maji, hurudi wenye mitungi mitupu, huona soni na masikitiko, hufunika vichwa vyao, kwani nchi imeatukaatuka; kwa kuwa haikuwako mvua katika nchi, wakulima huona soni, huvifunika vichwa vyao. Kwani kulungu nao wakizaa porini huwaacha watoto, kwa kuwa hakuna majani. Navyo vihongwe husimama vilimani juu, hutwetea upepo kama mbwa wa mwitu, macho yao huzimia kwa kuwa hakuna majani. Kweli manza, tulizozikora, zimetusuta; lakini, Bwana, yafanye yalipasayo Jina lako! Kwani tumekuacha mara nyingi, tukarudi nyuma, tumekukosea kweli. Wewe ndiwe, Waisiraeli wamngojeaye, ndiwe mwokozi wao, siku zinapokuwa mbaya. Mbona unataka kuwa kama mgeni katika nchi hii au kama mpitaji apigaye kambi tu kulala usiku? Mbona unataka kuwa kama mtu aliyeshindwa au kama fundi wa vita asiyeweza kuokoa? Wewe, Bwana, uko kwetu katikati, nasi huitwa kwa Jina lako, usituache! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya watu wa ukoo huu: Hupenda kwenda huko na huko, hawaizuii miguu yao; kwa hiyo Bwana hapendezwi nao, sasa anayakumbuka mabaya yao, waliyoyafanya, ayapatilize makosa yao. Naye Bwana akaniambia: Usiwaombee wao wa ukoo huu, niwafanyizie mema! Wakifunga mfungo, siwasikii malalamiko yao; hata wakitoa ng'ombe au vipaji vingine vya tambiko, sipendezwi nao. Kwani mimi nitawamaliza kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya. Nikasema: E Bwana Mungu, tazama! Wako wafumbuaji wanaowaambia: Hamtaona upanga, wala njaa haitakuwa kwenu, kwani nitawapa kutengemana kweli mahali hapa! Bwana akanijibu: Ni uwongo tu, hao wafumbuaji wanaofumbua katika Jina langu sikuwatuma, wala sikuwaagiza neno, wala sikusema nao. Wanayoyafumbua ni ndoto za uwongo na maaguaji ya bure na madanganyifu ya mioyo yao. Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Wafumbuaji hao wanaofumbua katika Jina langu mimi sikuwatuma, wao wanaosema: Hakuna upanga wala njaa itakayokuwa katika nchi hii, basi, wafumbuaji hao watamalizwa kwa panga na kwa njaa! Hata watu waliofumbuliwa nao watakuwa wametupwa barabarani mwa Yerusalemu wakiuawa kwa njaa na kwa panga, hatakuwako atakayewazika wao na wake zao na wana wao wa kiume na wa kike; ndivyo, atakavyowamwagia mabaya yao. Nawe na uwaambie neno hili: Macho yangu yanachuruzika machozi usiku na mchana, hayakomi, kwani wanawali walio wazaliwa wa ukoo wangu wamevunjika mavunjiko makuu, ni pigo lisilopona kabisa. Nikitoka kwenda shambani ninaona waliouawa na panga; nikiingia mjini ninaona waliozimia kwa njaa. Kwani nao wafumbuaji pamoja na watambikaji wanahamia nchi, wasiyoijua. Umemtupa Yuda kabisa? Roho yako imetapishwa na Sioni? Mbona umetupiga? Lakini hakuna atakayetuponya. Tunangojea utengemano, lakini hakuna chema; tunangojea siku za kupona, lakini tunayoyaona ni mastuko. Tunajua, Bwana, ya kuwa hatukukucha, tukakora manza, baba zetu walizozikora; kweli tumekukosea wewe. Lakini kwa ajili ya Jina lako usitukatae na kututweza! Usiache, kiti cha utukufu wako kibezwe! Likumbuke Agano lako, ulilolifanya na sisi, usilivunje! Je? Katika miungu ya wamizimu isiyo kitu imo iwezayo kunyesha mvua? Au ni mbingu zitoazo zenyewe manyunyu tu? Si wewe, Bwana Mungu wetu? Kwa hiyo tunakungojea, kwani wewe ndiwe ayafanyaye haya yote. Bwana akaniambia: Ijapo Mose na Samweli wanitokee, Roho yangu haitawaelekea wao wa ukoo huu. Waondoe usoni pangu, wajiendee! Kama wanakuuliza: Twende kwenda wapi? utawaambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kama ni kufa, nendeni kufa! Kama ni kuuawa na panga, nendeni kwenye panga! Kama ni kufa kwa njaa, nendeni kwenye njaa! Kama ni kutekwa, nendeni kutekwa! Nitawapatia namna nne za mapatilizo; ndivyo, asemavyo Bwana: Panga za kuwaua, mbwa wa kuwakokotakokota, ndege wa angani na nyama wa porini wa kuwala na kuwamaliza. Nitawatoa, watupwe huko na huko katika nchi zote zenye wafalme kwa ajili ya mambo yote, Manase, mwana wa Hizikia, mfalme wa Yuda, aliyoyafanya Yerusalemu. Yuko nani atakayekuhurumia, Yerusalemu? Yuko nani atakayekulilia? Au yuko nani atakayekufikia kukuuliza, kama unakaa vema? Ndivyo, asemavyo Bwana: Wewe umenitupa, ukarudi nyuma; ndipo, nilipoukunjua mkono wangu, ukukamate, nikakumaliza, maana nilikuwa nimechoka kuona uchungu. Kwa hiyo nimewapepeta ungoni kwenye malango ya nchi hii, nikawaua watoto wao, nikawaangamiza waliokuwa ukoo wangu, lakini hawakurudi katika njia zao. Nikiwahesabu wajane wao, ni wengi kuliko mchanga wa baharini; maana mwenye kuua mchana nimemleta kwao kwa mama wenye vijana, mara nikawaangushia mastuko na mashangao. Aliyezaa wana saba akazimia kwa uchungu, akakatika roho yake, kwa kuona soni na kujifunika jua lake likachwa, mchana ungaliko bado. Nayo masao yao nitayatoa, wauawe na panga za adui zao; ndivyo, asemavyo Bwana. Nilikuwa nimeapizwa, mama yangu aliponizaa! Nikawa mtu wa kugombezwa na wa kusutwa katika nchi hii yote nzima, nami sikukopesha wala sikukopa, nipate faida; nao wote huniapiza. Bwana amesema: Nitakutia nguvu kweli, uone mema! Kweli nitakupa kuwachokesha adui, siku zikiwa mbaya kwa kusongwa. Je? Yuko awezaye kuvunja chuma? kile chuma chenye shaba kitokacho kaskazini? Lakini kwanza nitazitoa mali zenu zote na vilimbiko vyenu vyote, wakunyang'anye pasipo kulipa cho chote kwa ajili ya makosa yenu yote, mliyoyafanya katika mipaka yenu yote. Nitawahamisha kwenda na adui zenu katika nchi, msiyoijua; kwani moto umewashwa na makali yangu, nao unataka kuwala. Bwana, wewe unanijua, nikumbuke! Unipatilizie na kunilipizia wanaonikimbiza! Usiwavumilie! Nipokee mimi! Ujue, ya kuwa ninatukanwa kwa ajili yako! Maneno yako yalipooneka yalikuwa chakula changu; hayo maneno yako yakaufurahisha moyo wangu na kuuchangamsha. Kwani ninakwita kwa Jina lako, Bwana uliye Mungu Mwenye vikosi. Sikukaa kwenye wafyozaji kucheka nao; kwa kushikwa na mkono wako nilikaa peke yangu, kwani walinijaza machafuko. Mbona maumivu yangu hayakomi? Mbona kidonda changu ni kibaya sana kwa kukataa kupona? Utaniwia kama kijito kidanganyacho au kama maji yasiyotegemeka? Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Utakaporudi, ndipo, nitakapokurudisha, usimame tena usoni pangu! Nao wapaswao na macheo utakapowatoa kwao wasiofaa, ndipo, utakapokuwa kama kinywa changu, ndipo, wale watakaporudi upande wako, wewe usiporudi upande wao. Nami nitakupa kuwawia wao wa ukoo huu boma la shaba lenye nguvu, wasikushinde wakikupelekea vita, kwani mimi niko pamoja na wewe, nikuokoe na kukuponya; ndivyo, asemavyo Bwana. Nitakuponya mikononi mwao wabaya, nitakukomboa mikononi mwao wakorofi. Neno la Bwana likanijia kwamba: Usijichukulie mke, usizae wana wa kiume wala wa kike mahali hapa! Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya wana wa kiume na wa kike wanaozaliwa mahali hapa na kwa ajili ya mama zao waliowazaa na kwa ajili ya baba zao waliowazaa katika nchi hii: Watakufa kwa magonjwa mabaya, hawataombolezewa, wala hawatazikwa, ila watakuwa tu kama kinyesi juu ya nchi; wengine watauawa kwa panga na kwa njaa, nayo mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani na cha nyama wa porini. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Usiingie nyumbani mwenye maombolezo, wala usiende kuwalilia, wala usiwakalie matanga! Kwani nimeuondoa utengemano wangu kwao walio ukoo huu, nisiwagawie chema, wala nisiwahurumie; ndivyo, asemavyo Bwana. Watakufa wakubwa na wadogo katika nchi hii pasipo kuzikwa, tena hakuna watakaowalilia wala watakaojikata chale wala watakaonyoa vichwa. Wala hakuna watakaowagawia vyakula, wakikaa matanga, wala watakaowatuliza mioyo kwa ajili ya mfu, wala hakuna watakaowanywesha vikombe vya kuwatuliza mioyo wakifiwa na baba au mama. Namo nyumbani mwenye karamu usimwingie kukaa nao, mkila, mkinywa! Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mtaniona na macho yenu siku hizi zenu, nikikomesha mahali hapa sauti za vicheko na sauti za furaha, hata sauti za wachumba wa kiume na wa kike. Itakuwa, utakapowapasha wao wa ukoo huu habari hizi zote, watakuuliza: Kwa sababu gani Bwana anatutakia haya mabaya yote yaliyo makuu? Tumekora manza gani? Bwana Mungu wetu, tumekosa makosa gani? Ndipo, utakapowaambia: Ndivyo, asemavyo Bwana: Kwa kuwa baba zenu waliniacha, wakafuata miungu mingine, wakaitumikia na kuiangukia, lakini mimi waliniacha, hawakuyashika Maonyo yangu. Nanyi hamkufanya mabaya kuliko baba zenu? Ninawaona, mkiufuata kila mtu ushupavu wa moyo wake mbaya pasipo kunisikia mimi. Kwa hiyo nitawaondoa katika nchi hii na kuwabwaga katika nchi, msiyoijua ninyi wala baba zenu! Ndiko, mtakakoweza kuitumikia miungu mingine mchana na usiku, kwa kuwa sitaki kuwahurumia tena. Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona kweli, siku zikija, watu watakapoacha kuapa wakisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyewatoa wana wa Isiraeli katika nchi ya Misri! Ila wataapa wakisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyewatoa wana wa Isiraeli katika nchi ya upande wa kaskazini na katika nchi zote, alikowatupia! Maana nitawarudisha katika nchi yao, niliyowapa baba zao. Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona, nikituma wavuvi wengi, wawavue! Kisha nitatuma wawinda wengi, wawawinde katika milima yote na katika vilima vyote na katika nyufa zota za miamba. Kwani macho yangu huziona njia zenu zote, hazifichiki usoni pangu, wala manza zao, walizozikora, hazifunikiki machoni pangu. Lakini kwanza nitawalipisha mara mbili manza zao na makosa yao, kwa kuwa wameichafua nchi yangu kwa mizoga ya matapisho yao, fungu langu wakalijaza machukizo yao. Bwana ndiwe nguvu yangu na ngome yangu na kimbilio langu siku ya masongano; wewe watakujia wamizimu wakitoka mapeoni kwa nchi, watakuambia: Baba zetu waliyokuwa nayo, ni mambo ya uwongo tu yasiyo maana, yasiyowafalia kitu. Je? Mtu atawezaje kujitengenezea miungu? Kweli siyo miungu! Mtaona kweli, nikiwajulisha mara hii, nikiwapa kuujua mkono wangu na uwezo wangu; ndipo, watakapojua, ya kuwa Jina langu ni Bwana. Ukosaji wa Yuda umeandikwa kwa kalamu ya chuma yenye ncha kali kama ya jiwe la almasi; mbao ulimochorwa ni mioyo yao na pembe za meza za kutambikia. Kwa hiyo wana wao huzikumbuka meza zao za kutambikia na vinyago vyao vya Ashera, wanapoona mti wenye majani mengi au wanapofika vilimani juu. Mlima wangu ulioko shambani na mali zako na vilimbiko vyako vyote vilivyoko vilimani nitavitoa, vipokonywe, kwa ajili ya makosa yako, uliyoyakosa katika mipaka yako yote. Nawe kwa ajili yako mwenyewe huna budi kulihama fungu lako, nililokupa, nami nitakutumikisha, uwatumikie adui zako katika nchi, usiyoijua, kwani makali yangu nimeyawakisha moto, usizimike kale na kale. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ameapizwa kila mtu amwegemeaye mtu mwenziwe akimtumia mwenye mwili kuwa mkono wake na kumwondoa Bwana moyoni mwake! Atakuwa kama mti wa jangwani usio na majani, hataona jema lo lote, likimjia; atakaa nyikani pakavu penyewe penye chumvi, pasipokaa mtu. Amebarikiwa kila mtu amwegemeaye Bwana, Bwana akiwa egemeo lake! Atakuwa kama mti uliopandwa penye maji upelekao mizizi yake mpaka mtoni; hauogopi, ijapo jua kali liufikie; majani yake hustawi vivyo hivyo; ijapo mwaka ukose mvua, hausumbuki, wala haukomi kuzaa matunda. Moyo wa mtu hudanganya kuliko mengine yote, tena huponza; yuko nani aujuaye? Mimi Bwana ninauumbua moyo nikiyajaribu mafigo, nimpe kila mtu yazipasayo njia zake na mapato ya matendo yake. Kama kwale anayelalia mayai, asiyoyataga, ndivyo, alivyo apataye mali kwa kupotoa watu; siku zake zitakapofika kati, zitampotelea, naye mwisho atapumbaa tu. Wewe kiti chenye utukufu umetukuka tangu mwanzo, ndipo mahali petu patakatifu, wewe Bwana u kingojeo cha Waisiraeli; wote wakuachao hupatwa na soni, waondokao kwako huandikwa wakingaliko nchini, ya kuwa wamemwacha Bwana aliye kisima chenye maji ya uzima. Niponye, Bwana! Ndivyo, nitakavyopona. Niokoe! Ndivyo, nitakavyookoka; kwani wewe ndiwe shangilio langu. Watazame wanaoniambia: Neno lake Bwana liko wapi? Na lije! Mimi sikujitoa katika uchungaji, nisikufuate, wala sikutaka, siku yenye uchungu iwajie, kama wewe unavyojua; yaliyotoka midomoni mwangu yako wazi usoni pako. Usiniangamize, wewe uliye kimbilio langu, siku ikiwa mbaya! Na wapatwe na soni wanikimbizao, nisipatwe na soni mimi! Na waangamie wao, nisiangamie mimi! Uwaletee wao siku mbaya! Mara mbili uwavunje, wavunjike kweli! Hivi ndivyo, Bwana alivyoniambia: Nenda kusimama langoni mwao walio wazaliwa wa ukoo huu, wafalme wa Yuda walimopitia wakiingia au wakitoka, hata malangoni mote mwa Yerusalemu, kawaambie: Lisikieni neno la Bwana, ninyi wafalme wa Yuda nanyi Wayuda nyote nanyi nyote mkaao Yerusalemu mnaopitia humu malangoni! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ziangalieni roho zenu, msichukue mzigo siku ya mapumziko mkiuingiza humu malangoni mwa Yerusalemu! Wala msitoe mzigo nyumbani mwenu siku ya mapumziko! Wala msifanye kazi yo yote! Ila itakaseni siku ya mapumziko, kama nilivyowaagiza baba zenu! Lakini hawakusikia, wala hawakuyatega masikio yao, wakazishupaza kosi zao, wasisikie, wasionyeke. Ndivyo, asemavyo Bwana: Sasa ninyi nisikieni, msiingize mzigo malangoni mwa mji huu siku ya mapumziko! Ila itakaseni siku ya mapumziko, msipoifanyizia kazi yo yote! Ndipo, watakapoingia humu malangoni mwa mji huu wafalme wanaokikalia kiti cha kifalme cha Dawidi na wakuu wanaopanda magari na farasi, wao wenyewe na wakuu wao, Wayuda nao wakaao Yerusalemu, nao mji huu utakaa kale na kale. Tena watakuja wakitoka katika miji ya Yuda na katika nchi zizungukazo Yerusalemu na katika nchi ya Benyamini, kwenye mbuga na kwenye milima, hata upande wa kusini, wataleta ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kuchinjwa na vipaji vingine vya tambiko na uvumba, wataviingiza Nyumbani mwa Bwana, wamshukuru. Lakini msiponisikia mkiacha kuitakasa siku ya mapumziko, mkaingia malangoni mwa Yerusalemu na kuchukua mizigo siku ya mapumziko, basi, nitawasha moto malangoni mwake, nao utayala majumba ya Yerusalemu pasipo kuzimika. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwake Bwana kwamba: Inuka, ushuke kwenda nyumbani mwa mfinyanzi. Ndimo, nitakamokuambia maneno yangu. Nikashuka kwenda nyumbani mwa mfinyanzi, nikamkuta, akifanya kazi kwenye kibao chake. Chombo, mfinyanzi alichokifanya na mkono wake, kisipokuwa chema, basi, akakitengeneza kuwa chombo kingine, kama ilivyofaa machoni pake mfinyanzi kukifanya. Neno lake Bwana likanijia kwamba: Kama huyu mfinyanzi nami siwezi kuwafanyizia ninyi mlio mlango wa Isiraeli? ndivyo, asemavyo Bwana. Tazameni: kama udongo ulivyo mkononi mwa mfinyanzi. ndivyo, ninyi mlio mlango wa Isiraeli mlivyo mkononi mwangu. Mara ninatisha taifa au ufalme kwamba: Nitawang'oa na kuwavunja na kuwaangamiza. Lakini taifa hilo, nililolitisha, likigeuka na kuuacha ubaya wake, nami nitageuza moyo, nisiwafanyizie hayo mabaya, niliyoyawaza kuwafanyizia. Mara ninaagiza taifa au ufalme kuwajenga na kuwapanda Lakini wakifanya yaliyo mabaya machoni pangu, wasiisikie sauti yangu, basi, nitageuza moyo, nisiwafanyizie hayo mema, niliyoyasema, niwafanyizie. Sasa uwaambie walio Wayuda nao wakaao Yerusalemu kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazameni, mimi ninawatengenezea mabaya kwa kuwawazia mawazo! Kwa hiyo rudini kila mtu katika njia yake mbaya, mshike njia zitakazowafaa, mfanye matendo mema! Lakini hujibu: Ni kazi bure! Kwani tutaendelea kuyafuata mawazo yetu, tufanye kila mtu yaupasayo ushupavu wa moyo wake mbaya! Kwa hiyo Bwana anasema hivyo: Ulizeni kwa wamizimu, kama yuko aliyesikia mambo kama hayo! Wanawali wa Isiraeli wamefanya mambo yazizimuayo kabisa. Je? Theluji ya Libanoni inaondoka katika ile miamba iliyoko kileleni juu ya kondeni? Je? Yanakauka maji yenye baridi ya vijito vitokavyo mbali? Lakini walio ukoo wangu wamenisahau, huvukizia miungu isiyo kitu, nayo ikawaangusha katika njia zao, walizozishika tangu kale, wakafuata mikondo isiyotengenezwa kuwa njia. Wakaigeuza nchi yao kuwa mapori tu, izomelewe kale na kale; kila atakayeipita ataistukia, wataitingishia vichwa vyao. Kama upepo utokao maawioni kwa jua unavyofanya, nitawatawanya machoni pa adui; ndio mgongo, sio uso, nitakaowaonyesha siku ya kuangamia kwao. Wakasema: Njoni, tumlie Yeremia njama ya kumwazia mawazo! Kwani maonyo hayampotelei mtambikaji, wala mizungu haimpotelei mjanja, wala maneno hayampotelei mfumbuaji. Haya! Tumpige tukiyatumia, ulimi wake uliyoyasema! Tusiyasikilize maneno yake yote! Bwana, nisikilize! Isikie sauti ya wapingani wangu! Je? Mema yanalipwa na kufanyiziwa mabaya? Wamenichimbia mwina; kumbuka, jinsi nilivyosimama mbele yako na kuwasemea mema, niyatulize makali yako yenye moto, yasiwatokee! Kwa hiyo watoe wana wao, wauawe na njaa, kawabwage kwenye panga, wanawake wao wawe pasipo watoto na pasipo waume! Waume wao na wauawe na kifo, vijana wao na wapigwe na panga za vitani! Nyumbani na msikilike vilio, ukiwastusha kwa kuwaletea vikosi vya wapiga vita! Kwani wamenichimbia mwina, wanikamate, miguu yangu wakaitegea matanzi. Wewe Bwana, unaijua njama yao yote ya kuniua; usizifunike manza zao, wala usiyafute makosa yao usoni pako, wawe wameangushwa usoni pako! Siku, makali yako yatakapowakia, wapigie shauri! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nenda, ujinunulie mtungi kwa mfinyanzi! Kisha chukua wazee wa watu na wazee wa watambikaji, utoke nao kwenda katika bonde la Mwana wa Hinomu lililoko mbele ya Lango la Vigae, utangaze huko maneno, nitakayokuambia! Uwaambie: Lisikilizeni neno la Bwana, ninyi wafalme wa Yuda nanyi mkaao Yerusalemu! Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaniona, nikipaletea mahali hapa mabaya; kila atakayeyasikia masikio yake yatavuma. Ni kwa sababu wameniacha, mahali hapa wakampa mgeni, wakavukizia hapa miungu mingine, wasiyoijua wenyewe, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda, wakapajaza mahali hapa damu zao wasiokosa. Wakamjengea Baali pa kumtambikia vilimani juu, wateketeze wana wao motoni kuwa ng'ombe za tambiko za Baali; nami sikuwaagiza hivyo, wala sikuvisema nao, wala havikunijia moyoni. Kweli ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, mahali hapa pasiitwe tena Tofeti wala Bonde la Mwana wa Hinomu, ila Bonde la Uuaji. Ndipo, nitakapoiumbua miungu ya Wayuda na ya Wayerusalemu mahali hapo nikiwatoa, waangushwe na panga machoni pa adui zao kwa mikono yao waliozitafuta roho zao, nayo mizoga yao nitawapa ndege wa angani na nyama wa porini, iwe chakula chao. Nao mji huu nitaugeuza kuwa mapori tu, uzomelewe kabisa; kila atakayepapita ataustukia, atauzomea kwa ajili ya mapigo yake yote. Nitawalisha nyama za wana wao wa kiume na nyama za wana wao wa kike, watazila kila mtu nyama za mwenziwe kwa kusongeka na kwa kuhangaika, adui zao wanaozitaka roho zao wakiwahangaisha. Kisha utauvunja mtungi machoni pao waume waliokwenda na wewe, ukiwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Hivi ndivyo, nitakavyowavunja walio wa ukoo huu nao mji huu, kama mtu anavyokivunja chombo cha mfinyanzi kisichowezekana kuwa kizima tena. Nako Tofeti ndiko, watakakozikia, kwa kukosa pengine pa kuzikia. Ndivyo, asemavyo Bwana: Hivi ndivyo, nitakavyopafanyizia mahali hapa nao wakaao hapa nitakapoutoa mji huu, uwe kama Tofeti. Ndipo, nyumba za Yerusalemu na nyumba za wafalme wa Yuda zitakapokuwa zimetiwa uchafu kama mahali pa Tofeti, Zitakazokuwa hivyo ni nyumba zote, walimovukizia vikosi vyote vya mbinguni madarini juu, walimomwagia miungu mingine vinywaji vya tambiko. Yeremia aliporudi toka Tofeti, Bwana alikomtuma kuwafumbulia watu, akaja kusimama uani pake Nyumba ya Bwana, akawaambia watu wote waliokuwako: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaniona, nikiuletea mji huu navyo vijiji vyake vyote mabaya yote, niliyoyasema, kwani wamezishupaza kosi zao, wasiyasikie maneno yangu. Mtambikaji Pashuri, mwana wa Imeri, aliyekuwa msimamizi mkuu wa Nyumba ya Bwana, akamsikia Yeremia, alipoyafumbua maneno yale. Ndipo, Pashuri alipompiga mfumbuaji Yeremia, akamfunga kwa mikatale iliyokuwa kwenye lango la juu la Benyamini katika Nyumba ya Bwana. Kulipokucha Pashuri akamfungua Yeremia tena katika mikatale; ndipo, Yeremia alipomwambia: Bwana hatakuita tena jina lako Pashuri, ila Magori-Misabibu (Kitisho po pote). Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Utaniona, nikikutoa kuwa kitisho kwako wewe nako kwao wote wakupendao, maana wataangushwa kwa panga za adui zao, nayo macho yako yataviona! Nao Wayuda wote nitawatia mkononi mwa mfalme wa Babeli, atawahamisha kwenda Babeli akiwapiga kwa upanga. Nazo mali zote za mji huu nitazitoa, na mapato yao yote na vitu vyao vyote vyenye kiasi kikubwa na vilimbiko vyote vya mfalme wa Yuda, nitavitia mikononi mwa adui zao, wavipokonye, wavichukue na kuvipeleka Babeli. Wewe Pashuri nawe nao wote wakaao nyumbani mwako mtakwenda kwa kutekwa, utafika Babeli, utakufa huko, utazikwa huko wewe na wapenzi wako wote, uliowafumbulia maneno ya uwongo. Bwana umenishinda, nami nimeshindika; umenishika kwa nguvu, ukaniweza. Ninachekwa mchana kutwa, wote wananifyoza. Kwani ninaposema ninalia; sina budi kutangaza ukorofi na upotovu, kwani Neno la Bwana hunipatia kutukanwa na kufyozwa mchana kutwa. Kwa hiyo nilisema: Sitamkumbuka, wala sitasema tena katika Jina lake, basi, ikawa moyoni mwangu kama moto uwakao kwa kufungiwa katika mifupa yangu, nikashindwa kuuvumilia, sikuweza kabisa. Kwani nimesikia wengi, wakinong'onezana kwamba: Anatishwa po pote, mchongeeni! Nasi na tumchongee! Hiyo ni njama yao wote walio rafiki zangu, hunivizia, nianguke, kwamba: Labda atashindwa, tumweze nasi, tupate kujilipiza kwake. Lakini Bwana yuko pamoja nami kama mpiga vita mwenye nguvu; kwa hiyo wanikimbizao watajikwaa, wasiniweze, watapatwa na soni kabisa, kwani hawaerevuki, soni zao zitakuwa za kale na kale, hazitasahauliwa. Wewe Bwana unajaribu mwongofu, unayaona mafigo na moyo; na nione, jinsi unavyowalipiza kisasi, kwani nimekusukumia wewe shauri langu. Mwimbieni Bwana! Mshangilieni Bwana! Kwani huiponya roho ya mkiwa mikononi mwao wafanyao mabaya. Siku niliyozaliwa iwe imeapizwa! Siku, mama yangu aliyonizaa, isibarikiwe! Awe ameapizwa naye mtu aliyempasha baba yangu habari kwamba: Umezaliwa mtoto wa kiume! akamfurahisha. Mtu huyo na awe kama ile miji, Bwana aliyoiangamiza pasipo kugeuza moyo! Asubuhi na asikie vilio, tena makelele, jua linapofika kichwani, kwa kuwa hakunifisha tumboni mwa mama; hivyo mama angalikuwa kaburi langu, hiyo mimba yake ingalikuwa ya siku zote. Mbona nilitoka tumboni kuona masumbufu na machungu, siku zangu zikamalizika, nikipatwa na soni tu? Hili ndilo neno lililotoka kwa Bwana, likamjia Yeremia, mfalme Sedekia alipomtuma Pashuri, mwana wa Malkia, na mtambikaji Sefania, mwana wa Masea, kwenda kwake kwamba: Mwulize Bwana kwa ajili yetu, kwani Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, ametuletea vita. Labda Bwana atatufanyizia nasi, kama mataajabu yake yote yalivyo, akiwaondoa kwetu. Yeremia akawaambia: Hivi ndivyo, mmwambie Sedekia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mtaniona, nikivirudisha vyombo vya vita vilivyo mikononi mwenu, mlivyovitumia kupiga vita na mfalme wa Babeli na Wakasidi wanaowasonga! Nitavitoa huko nje, nivilete kwenye boma, kisha nitavikusanya humu mjini katikati. Nami mwenyewe nitapigana nanyi kwa kiganja kilichofumbuka cha mkono ulio wenye nguvu kwa kuwa na makali yenye moto na machafuko makubwa. Nitawatoa wakaao humu mjini, watu hata nyama, watakufa kwa ugonjwa mbaya uuao kabisa. Ndivyo, asemavyo Bwana: Hayo yatakapokwisha, nitamtoa Sedekia, mfalme wa Yuda, pamoja na watumishi wake nao walio wa ukoo huu waliosalia humu mjini kwa ule ugonjwa mbaya na kwa panga na kwa njaa, nitawatia mikononi mwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, nami mikononi mwa adui zao namo mikononi mwao wanaozitafuta roho zao, naye atawapiga kwa ukali wa upanga, hatawaonea uchungu, wala hatawachagulia, wala hatawahurumia. Nao walio wa ukoo huu utawaambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nitazameni! Ninalinganya machoni penu njia ya uzima na njia ya kufa. Atakayekaa humu mjini atakufa kwa upanga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya. Lakini atakayetoka na kuwaangukia Wakasidi wanaowasonga atapona, nayo roho yake itakuwa pato lake. Kwani nimeuelekeza uso wangu kwenye mji huu, niupatie mabaya, mema siyo; utatiwa mkononi mwake mfalme wa Babeli, auteketeze kwa moto; ndivyo, asemavyo Bwana. Nao wa mlango wa mfalme wa Yuda waambie: Lisikieni neno la Bwana! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ninyi wa mlango wa Dawidi, asubuhi pigeni mashauri, mwaponye walionyang'anywa mkiwatoa mikononi mwa wakorofi, makali yangu yasitokee kuwa moto uwakao, asipopatikana mwenye kuuzima kwa ajili ya ubaya wa matendo yenu! Ndivyo, asemavyo Bwana: Utaniona, nikikujia wewe ukaaye bondeni, uliye kama mwamba mbugani. Ninyi husema: Yuko nani atakayetushukia? Yuko nani atakayeingia katika makao yetu? Mimi nitawapatiliza, kama matendo yenu yalivyowapatia; ndivyo, asemavyo Bwana. Nitawasha moto mwituni kwao utakaozila nchi zote ziwazungukazo. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Shuka kwenda nyumbani mwa mfalme wa Yuda, uliseme mle neno hili, kwamba: Sikia, mfalme wa Yuda, ukikaliaye kiti cha kifalme cha Dawidi, wewe na watumishi wako nao walio wa ukoo wako mnaoingia humu malangoni! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Fanyeni yaliyo sawa yaongokayo! Waponyeni walionyang'anywa na kuwatoa mikononi mwa wakorofi! Wageni nao waliofiwa na wazazi na wajane msiwaonee, wala msiwakorofishe! Wala damu zao wasiokosa msizimwage mahali hapa! Kwani kama mtalifanya kweli neno hili, wataingia malangoni mwa nyumba hii wafalme wanaokikalia kiti cha kifalme cha Dawidi, wanaopanda magari na farasi, wao wenyewe na watumishi wao na watu wao. Lakini msipoyasikia maneno haya, basi, nimejiapia mwenyewe, nyumba hii itakuwa mavunjiko; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyoisemea nyumba ya mfalme wa Yuda: Kwangu wewe u kama Gileadi ulio mlima mkubwa wa Libanoni; kweli nitakugeuza kuwa nyika yenye miji isiyokaa watu. Nitajichagulia waangamizaji wako, kila mtu na mata yake, waikate miangati yako iliyochaguliwa, waitupe motoni! Wamizimu wengi watakapopapitia penye mji huu wataulizana mtu na mwenziwe: Kwa sababu gani Bwana ameufanyizia mji huu mkubwa mambo kama hayo? Nao watu watawajibu: Ni kwa sababu wameliacha Agano la Bwana Mungu wao, wakaangukia miungu mingine na kuitumikia. Msimlilie mfu, wala msimwombolezee! Ila mmlilie sana yeye aliyekwenda! Kwani hatarudi tena, wala hataiona tena nchi, alikozaliwa. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya Salumu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, aliyempokea baba yake ufalme, akatoka mahali hapa: Hatarudi huku tena! Kwani mahali, walipomhamishia, ndipo, atakapofia, asiione tena nchi hii. Yatampata aijengaye nyumba yake kwa njia isiyoongoka, navyo vyumba vyake vilivyomo kwa njia isiyo sawa; huzitumia kazi za mwenziwe bure tu asipompa mshahara wake. Anasema: Nitajijengea nyumba kubwa yenye vyumba vipana, nitavitobolea madirisha, nitavipigilia juu mbao za miangati, kisha nitavipaka rangi nyekundu. Je? Ufalme wako ni kushindana na miangati? Je? Baba yako hakula, hakunywa? Lakini amefanya yaliyo sawa yaongokayo; ndipo, alipopata kukaa vema. Akatengenezea wanyonge na wakiwa mashauri yao; ndipo, alipopata kukaa vema; huko siko kunijua? ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani hakuna mengine, macho yako na moyo wako yanayoyatazamia, ni njia tu za kupata, nazo za kumwaga damu zao wasiokosa, nazo za kukorofisha, nazo za kupenyezewa, uyafanye mambo hayo. Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda: Hawatamwombolezea kwamba: A ndugu yetu! A umbu letu! Wala hawatamwombolezea kwamba: A bwana! A mwenye utukufu! Atazikwa, kama punda anavyozikwa, akikokotwa na kutupwa nje kwenye malango ya Yerusalemu. Panda Libanoni, ulie! Nako Basani zipaze sauti zako! Nako toka Abarimu vilio vyako visikilike! Kwani wote waliokupenda wamepondwa. Nilikuambia neno, ulipokuwa umetulia vema, ukajibu: Sisikii! Hii ndiyo njia yako tangu ujana wako, kwani hukuisikia sauti yangu. Upepo utawachunga wachungaji wako wote, nao waliokupenda watakwenda kufungwa; ndipo, utakapoona soni na kuiva uso kwa ajili ya ubaya wako wote. Unakaa kama ndege ya Libanoni katika tundu kwenye miangati; lakini utapaswa na kuhurumiwa, machungu yatakapokujia yatakayokuwa kama uchungu wa mzazi. Ndivyo, asemavyo Bwana: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, kama wewe Konia, mwana wa Yoyakimu, mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yenye muhuri mkononi pangu pa kuume, ningekuondoa kwa nguvu, nikakutia mikononi mwao waitafutao roho yako namo mikononi mwao, unaowaogopa sana, namo mikononi mwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, namo mikononi mwa Wakasidi. Tena wewe na mama yako aliyekuzaa nitawabwaga katika nchi nyingine isiyo yenu ya kuzaliwa; ndiko, mtakakofia. Lakini katika nchi hii, wanayoitunukia rohoni mwao, hawatarudi huku. Je? Huyu mtu Konia siye chungu kinachowaziwa si kitu, kinachovunjwa tu? Siye chombo kisichopendwa? Mbona yeye nao walio kizazi chake wamebwagwa na kutupwa katika nchi, wasiyoijua? E nchi, nchi, nchi, lisikie Neno lake Bwana! Ndivyo, Bwana anavyosema: Mwandikeni mtu huyu kuwa pasipo watoto, kuwa mtu asiyejipatia mema siku zake zote, hata katika kizazi chake hamna mtu atakayejipatia kukikalia kiti cha kifalme cha Dawidi na kuwatawala Wayuda tena. Yatawapata wachungaji wanaowaangamiza na kuwatawanya kondoo, niliowapa kuwachunga! ndivyo, asemavyo Bwana. Hivi ndivyo kweli, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema kwa ajili ya wachungaji. Ninyi mnaowachunga walio ukoo wangu, mmewatawanya kondoo wangu na kuwakimbiza, hamkuwaangalia; mtaniona, nikiwapatilizia ubaya wa matendo yenu; ndivyo, asemavyo Bwana. Nami nitawakusanya masao ya kondoo wangu na kuwatoa katika nchi zote, nilikowaendesha na kuwakimbiza, Nitawarudisha katika makao yao, wazae, wawe wengi tena. Kisha nitawawekea wachungaji, wawachunge; hawataogopa tena, wala hawatastuka, wala hawatapotea hata mmoja wao; ndivyo, asemavyo Bwana. Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zitakapokuja, nikimwinulia Dawidi chipuko lenye wongofu, naye atakuwa mfalme ajuaye vema kutawala, maana atafanya katika nchi yaliyo sawa yaongokayo. Yuda ataokolewa katika siku zake, naye Isiraeli atakaa salama. Jina lake, watakalomwita, ni hili: Bwana ni wongofu wetu! Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona kweli, siku zikija, watakapoacha kuapa wakisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyewatoa wana wa Isiraeli katika nchi ya Misri, ila wataapa wakisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyewaleta wazao wa mlango wa Isiraeli akiwatoa katika nchi ya upande wa kaskazini na katika nchi zote, nilikowaendesha na kuwakimbiza; ndipo, watakapokaa huku katika nchi yao. Kwa wafumbuaji. Moyo wangu umevunjika kifuani mwangu, mifupa yangu yote ikatetemeka; nikawa kama mlevi au kama mtu ashindwaye na mvinyo, nilipoyasikia yaliyotoka kwake Bwana, hayo maneno yake matakatifu kwamba: Nchi hii imezaa wazinzi, kwa hiyo nchi hii inakaa matanga kwa kuapizwa, mbuga za nyikani zimekauka, kwa kuwa ni mabaya, wanayoyakimbilia, nayo nguvu yao siyo ifaayo. Kwani nao wafumbuaji pamoja na watambikaji ni wapotovu, namo Nyumbani mwangu nimeuona ubaya wao; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwa sababu hii njia yao itakuwa inateleza, penye giza watateleza na kuanguka hapohapo, kwani nitawaletea mabaya, ndio mwaka wa kupatilizwa kwao; ndivyo, asemavyo Bwana. Hata kwa wafumbuaji wa Samaria nimeona upumbavu, wakifumbua kwa nguvu ya Baali, wakawapoteza nao walio ukoo wangu wa Isiraeli. Lakini kwa wafumbuaji wa Yerusalemu nimeona mastusho: huzini, huendelea na kudanganya, huitia mikono ya wabaya nguvu, wasiuache kila mtu ubaya wake, wote pia wameniwia kama Wasodomu, nao wakaao humo kama Wagomora. Kwa hiyo Bwana Mwenye vikosi anasema hivyo kwa ajili ya wafumbuaji: Mtaniona, nikiwalisha majani machungu na kuwanywesha maji yenye sumu! Kwani kwa wafumbuaji wa Yerusalemu kumetoka upotovu, ukaziingia nchi zote. *Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Msiyasikie maneno ya wafumbuaji wanaowafumbulia maneno wakiwaegemeza mambo yaliyo ya bure tu! Huyasema, waliyoyaona mioyoni mwao, hawasemi yaliyotoka kinywani mwa Bwana. Huwaambia wanibezao: Bwana amesema: Mtakaa na kutengemana! Kila mtu aufuataye ushupavu wa moyo wake humwambia: Hakuna kibaya kitakachowafikia! Kwani yuko nani aliyesimama penye njama ya Bwana, akimwona au akilisikia neno lake? Yuko nani aliyeliangalia Neno lake, akilisikia? Mtakiona kimbunga cha Bwana, hata makali yenye moto, yakitoka kwake, nao upepo wa chamchela wenye nguvu utawaangukia vichwani wao wasiomcha Mungu. Ukali wake Bwana hautatulia, mpaka ukiyafanya na kuyatimiza mawazo ya moyo wake; siku za mwisho mtayatambua haya. Sikuwatuma wafumbuaji hawa, nao hupiga mbio; sikuwaambia neno, nao hufumbua. Kama wangalikuwa wamesimama penye njama yangu, wangeyasema maneno yangu masikioni pao walio ukoo wangu, wangewarudisha wabaya katika njia zao, wauache ubaya wa matendo yao. Ndivyo asemavyo Bwana: Je? Mimi ni Mungu akaaye karibu tu? Si Mungu akaaye hata mbali? Ndivyo, asemavyo Bwana: Kama mtu anajificha mafichoni, mimi sitamwona? Si mimi azijazaye mbingu na nchi? ndivyo, asemavyo Bwana. Nimeyasikia, wafumbuaji waliyoyasema, wakifumbua maneno ya uwongo katika Jina langu wakisema: Nimeota! Nimeota! Hivyo vitakuwa mpaka lini mioyoni mwao wafumbuaji wafumbuao uwongo tu, walio wafumbuaji wa udanganyifu wa mioyo yao? Huwaza, ya kuwa watawasahaulisha walio ukoo wangu Jina langu kwa ajili ya ndoto zao, wakizisimuliana kila mtu na mwenziwe, kama baba zao walivyolisahau Jina langu kwa ajili ya Baali. Mfumbuaji aliyeota na asimulie ndoto! Naye aliyelisikia Neno langu na aliseme Neno langu, lilivyo kweli! Kumvi na mpunga ziko na fungu gani lililo lao pamoja? ndivyo, asemavyo Bwana. Ndivyo, asemavyo Bwana: Neno langu si kama moto au kama nyundo ipasuayo miamba?* Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona kweli, nikiwajia wafumbuaji, kwa kuwa wanaliiba Neno langu kila mtu kwa mwenziwe! Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona, nikiwajia wafumbuaji, kwa kuwa huzitumia ndimi zao za kusema: Asema! Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona, nikiwajia wafumbuaji wa ndoto za uwongo. Huzisimulia walio ukoo wangu, wakawapoteza kwa uwongo wao na kwa mambo yao makuu, nami sikuwatuma, wala sikuwaagiza neno, nao walio wa ukoo huu hawawafalii kitu hata kidogo; ndivyo, asemavyo Bwana. Kama watakuuliza walio wa ukoo huu au mfumbuaji au mtambikaji kwamba: Tamko zito la Bwana ni nini? ndipo, utakapowajibu: Hili ndilo tamko zito la Bwana, akisema: Nitawabwaga ninyi! ndivyo, asemavyo Bwana. Lakini mfumbuaji na mtambikaji nao walio wa ukoo huu watakaolitumia neno hilo la kwamba: Tamko zito la Bwana, mtu huyo nitampatiliza pamoja na mlango wake. Hivyo ndivyo, mtakavyoulizana mtu na mwenziwe, hata mtu na ndugu yake kwamba: Bwana amejia nini? au: Bwana amesema nini? Tamko zito la Bwana wasilitaje tena! Kama wanalitaja, basi, kila mtu neno lake litamgeukia kuwa tamko zito, kwani ninyi huyageuza maneno ya Mungu aliye Mwenye uzima, aliye Bwana Mwenye vikosi, Mungu wetu. Hivi ndivyo, utakavyomwuliza mfumbuaji kwamba: Bwana amejibu nini? au: Bwana amesema nini? Lakini mkisema: Tamko zito la Bwana, basi, itakuwa hivyo, Bwana alivyosema: Kwa kuwa mnalisema neno hilo la kwamba: Tamko zito la Bwana, nami nilituma kwenu kuwakataza, msiseme: Tamko zito la Bwana! basi, mtaniona, nikiwaacha kabisa na kuwabwaga ninyi pamoja na mji huu, niliowapa ninyi na baba zenu, mtoke usoni pangu. Hivyo nitawatia soni za kale na kale na matusi ya kale na kale yasiyosahaulika. Bwana alinionyesha, nikaona vikapu viwili vyenye kuyu, vilikuwa vimewekwa mbele ya Jumba la Bwana, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alipokuwa amekwisha kumteka Yekonia, mwana wa Yoyakimu, mfalme wa Yuda, nao wakuu wa Yuda pamoja na mafundi wa seremala na wahunzi kuwatoa Yerusalemu na kuwapeleka Babeli. Kikapu kimoja kuyu zake zilikuwa nzuri kabisa, kama kuyu za malimbuko zilivyo; kikapu cha pili kuyu zake zilikuwa mbaya kabisa, hazikulika kwa ubaya wao. Bwana akaniuliza: Unaona nini, Yeremia? Nikamwambia: Kuyu; hizi kuyu nzuri ni nzuri kabisa, nazo hizi mbaya ni mbaya kabisa, haziliki kwa ubaya wao. Neno la Bwana likanijia kwamba: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli: Kama hizi kuyu nzuri zinavyopendeza, ndivyo, nitakavyowatazama kwa kupendezwa Wayuda waliotekwa, niliowatuma kutoka mahali hapa kwenda katika nchi ya Wakasidi. Nitayaelekeza macho yangu, yawaangalie kwa kupendezwa nao, nitawarudisha katika nchi hii, nitawajenga, nisiwabomoe tena, nitawapanda, nisiwang'oe tena. Nitawapa mioyo ya kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, watakuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wao, kwani watanigeukia kwa mioyo yote. Tena hivi navyo ndivyo, Bwana anavyosema: Kama zile kuyu zilivyo mbaya, zisilike kwa ubaya wao, ndivyo, nitakavyomtoa Sedekia, mfalme wa Yuda, na wakuu wake na masao ya Yerusalemu nao waliosalia katika nchi hii nao wakaao katika nchi ya Misri, nitawatoa, watupwe vibaya huko na huko katika nchi zote zenye wafalme huku ulimwenguni, watukanwe na kuzomelewa, wafyozwe na kuapizwa po pote, nitakapowatupa. Nitatuma kwao panga na njaa na magonjwa mabaya, mpaka watakapomalizika na kutoweka katika nchi, niliyowapa wao na baba zao. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kwa ajili ya ukoo wote wa Yuda katika mwaka wa nne wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, nao ulikuwa mwaka wa kwanza wa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli. Naye mfumbuaji Yeremia akaliambia wao wote wa ukoo wa Yuda nao wote wakaao Yerusalemu kwamba: Kuanzia mwaka wa kumi na tatu wa Yosia, mwana wa Amosi, mfalme wa Yuda, mpaka siku hii ya leo, hii miaka ishirini na mitatu yote neno la Bwana limenijia, nikawaambia pasipo kuchoka kila kulipokucha, lakini hamkusikia. Naye Bwana alituma kwenu watumishi wake wote waliokuwa wafumbuaji, naye aliwatuma pasipo kuchoka kila kulipokucha, lakini hamkusikia, wala hamkuyatega masikio yenu, mpate kusikia. Nao wakasema: Rudini kila mtu katika njia yake mbaya na kuyaacha matendo yenu mabaya! Ndipo, mtakapokaa katika nchi, Bwana aliyowapa ninyi na baba zenu, iwe yenu ya kale na kale kabisa. Msiifuate miungu mingine kuitumikia na kuiangukia, wala msinikasirishe kwa matendo ya mikono yenu, nisiwafanyizie mabaya. Lakini hamkunisikia, mkataka kunikasirisha kwa matendo ya mikono yenu, yakawapatia mabaya; ndivyo, asemavyo Bwana. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kwa kuwa hamkuyasikia maneno yangu, mtaniona, nikituma wa kuzichukua koo zote za watu wa upande wa kaskazini. Ndivyo, asemavyo Bwana: Nitatuma hata kwa mtumishi wangu Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, nitamleta katika nchi hii kuwapiga wakaao huku nayo mataifa haya yote ya nchi ziwazungukazo; nitawatowesha nikiwatoa, wamalizwe kabisa na kuzomelewa, pawe mavunjiko ya kale na kale. Nitapoteza kwao sauti za vicheko na sauti za furaha, hata sauti za wachumba wa kiume na wa kike, hata milio ya mawe ya kusagia, hata mwanga wa taa. Nchi hii yote itakuwa mavunjiko kwa kukaa peke yake. Nao watu wa mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka 70. Ndivyo, asemavyo Bwana: Itakuwa, miaka 70 itakapopita, nitampatilizia mfalme wa Babeli na lile kabila lote mabaya yao, waliyoyafanya; hata nchi yao Wakasidi nitaigeuza kuwa peke yake tu kale na kale. Nitailetea nchi ile maneno yangu yote, niliyoyasema ya kuifanyizia, yaliyoandikwa humu kitabuni, mfumbuaji Yeremia aliyoyafumbua kwamba: Yatawajia hawa wamizimu wote. Kwani mataifa yenye watu wengi na wafalme wakuu watawatumikisha hawa nao, nami nitawalipisha kazi zao na matendo ya mikono yao. Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli alivyoniambia: Kitwae mkononi mwangu kinyweo hiki cha mvinyo yenye ukali wa moto, ukinyweshe makabila yote ya watu, ambao nitakutuma kwenda kwao. Watakapokinywa watapepesuka kwa kuingiwa na wazimu kwa ajili ya upanga utakaotumwa kwao. Nikakitwaa hicho kikombe mkononi mwake Bwana, nikakinywesha makabila yote ya watu, ambao Bwana alinituma kwenda kwao. Yerusalemu na miji ya Yuda na wafalme wao na wakuu wao kikawapatia mavunjiko na maangamizo na mazomeo na maapizo, kama vilivyo hata leo. Kisha nikamnywesha Farao, mfalme wa Misri, na watumishi wake na wakuu wake na watu wake wote, nao wote waliochangana nao wafalme wote wa nchi ya Usi na wafalme wote wa nchi ya Wafilisti, hata Askaloni na Gaza na Ekroni na masao ya Asdodi, hata Waedomu na Wamoabu na wana wa Amoni, nao wafalme wote wa Tiro na wafalme wote wa Sidoni na wafalme wa nchi za pwani ng'ambo ya bahari, Wadedani na Watema na Wabuzi nao wote wakatao nywele za panjani, nao wafalme wote wa Arabuni na wafalme wote wa watu waliochangana nao wakaao nyikani, na wafalme wote wa Zimuri na wafalme wote wa Elamu na wafalme wa Wamedi, na wafalme wote wa nchi za upande wa kaskazini, walioko karibu nao walioko mbali, kila mtu na ndugu yake; hivyo nikawanywesha wote wenye nchi za kifalme zilizoko huku ulimwenguni; lakini mfalme wa Sesaki (Babeli) atakunywa nyuma yao wote. Nawe utawaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Nyweni, mpaka mlewe na kutapika! Mtaanguka, msiweze kuinuka tena kwa ajili ya upanga, mimi ninaotaka kuutuma kwenu. Kama wanakataa kukitwaa hicho kikombe mkononi mwako, wasikinywe, ndipo, utakapowaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Hamna budi kukinywa! Kwani mmeona, nilivyoanza kuufanyizia mabaya ule mji ulioitwa kwa Jina langu, nanyi mpone kabisa? Hamtapona, kwani upanga, ninaouita mimi, utawajia wote wakaao ulimwenguni; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Kisha wewe utawafumbulia maneno haya yote ukiwaambia: Bwana atanguruma huko juu na kupaza sauti yake katika Kao lake takatifu akiyangurumia malisho yake; atapiga yowe kama wakamuliaji wa zabibu atakapowajia watu wote wakaao huku ulimwenguni. Mlio wake utakwenda kufika mapeoni kwa nchi, kwani Bwana atawakatia makabila ya watu shauri lake, yeye atawahukumu wote wenye miili, nao wasiomcha atawatoa, wauawe na upanga ule; ndivyo, asemavyo Bwana. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mtaona, mabaya yakitoka kwa kabila moja kufikia jingine, nao upepo wenye nguvu nyingi utainuka mapeoni kwa nchi, utokee. Siku ile itakuwa, waliouawa na Bwana walale po pote toka mwanzo wa nchi kuufikia mwisho wa nchi, hawataombolezewa, wala hawataokotwa, wala hawatazikwa, watakuwa kinyesi tu juu ya nchi. Pigeni makelele, ninyi wachungaji, na kulia sana! Gaagaeni mavumbini, ninyi viongozi wa makundi! Kwani siku zenu zimetimia za kuchinjwa, nami nitawaponda, mwanguke chini kama chombo kilichopendeza. Ndipo, kimbilio litakapowapotelea wachungaji, nao viongozi wa makundi hawatapata pa kuponea. Sauti za vilio vya wachungaji na makelele ya viongozi wa makundi yatasikilika hapo, Bwana atakapoyaharibu malisho yao. Nazo mbuga zile nzuri za kutulia hapo zitakuwa kimya pasipo sauti yo yote kwa ajili ya moto wa makali yake Bwana. Atakuwa ametokea kama simba akiondoka kichakani. Kweli nchi yao itakuwa imegeuka kuwa mapori tu kwa ukali wa moto wa Mwenye nguvu, ndio moto wa makali yake. *Katika mwanzo wa ufalme wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, ndipo, neno hili lilipotoka kwake Bwana kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Simama uani pa Nyumba ya Bwana, nao watu wa miji yote watakaopaingia kutambika Nyumbani mwa Bwana uwaambie maneno yote, niliyokuagiza kuwaambia, usipunguze hata neno moja. Labda watasikia, warudi kila mmoja katika njia yake mbaya, nipate kugeuza moyo kwa ajili ya mabaya, niliyoyawaza kuwafanyizia kwa matendo yao mabaya. Nawe utawaambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msiponisikia, msipoendelea kuyashika Maonyo yangu, niliyowapa ninyi, yawe machoni penu, msipoyashika maneno ya wafumbuaji walio watumishi wangu, mimi ninaowatuma kwenu pasipo kuchoka kila kunapokucha, msipowasikia, nitaigeuza Nyumba hii kuwa kama Silo, nao mji huu nitautoa, uapizwe na mataifa yote yaliyoko ulimwenguni. Watambikaji na wafumbuaji na watu wote wa ukoo huu wakamsikia Yeremia, alipoyasema maneno haya katika Nyumba ya Bwana. Yeremia alipokwisha kuyasema yote, Bwana aliyomwagiza kuwaambia watu wote wa ukoo huu, ndipo, watambikaji na wafumbuaji na watu wote wa ukoo huu walipomkamata wakisema: Sharti ufe kabisa! Mbona umetufumbulia katika Jina la Bwana kwamba: Nyumba hii itakuwa kama Silo, nao mji huu utakuwa mavunjiko, usikae mtu? Kisha watu wote wa ukoo huu wakamkusanyikia Yeremia katika Nyumba ya Bwana. Wakuu wa Yuda walipoyasikia maneno haya wakatoka nyumbani mwa mfalme, wakapanda kwenda katika Nyumba ya Bwana, wakakaa kwenye mlango mpya wa Bwana. Watambikaji na wafumbuaji wakawaambia wakuu na watu wote wa ukoo huu, wakasema: Mtu huyu anapaswa na hukumu ya kuuawa, kwani mji huu ameufumbulia maneno, kama mlivyosikia ma masikio yenu. Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote wa ukoo huu, akasema: Bwana amenituma kuyafumbua hayo maneno yote yatakayoijia Nyumba hii na mji huu, mliyoyasikia. Sasa fanyeni mwenendo mwema na matendo mema mkiisikia sauti ya Bwana Mungu wenu! Ndipo, Bwana atakapogeuza moyo, asiwafanyizie hayo mabaya, aliyoyasema! Lakini mimi nitazameni! Nimo mikononi mwenu; nifanyizieni, mliyoyaona na macho yenu kuwa mema yanyokayo! Lakini jueni hili kabisa: Ninyi mtakaponiua mtafanya, damu ya mtu asiyekosa iwajie ninyi na mji huu nao wakaao humu! Kwani Bwana amenituma kweli kwenu kuyasema maneno haya masikioni penu.* Ndipo, wakuu na watu wote wa ukoo huu walipowaambia watambikaji na wafumbuaji: Mtu huyu hapaswi na hukumu ya kuuawa, kwani amesema na sisi katika Jina la Bwana. Kulikuwa na wazee wa nchi hii, wakainuka, wakauambia mkutano wote wa watu wa ukoo huu, wakasema: Mika wa Moreseti alikuwa mfumbuaji siku za Hizikiya, mfalme wa Yuda, akawaambia watu wote wa Yuda kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Sioni utalimwa kuwa shamba, nao Yerusalemu utageuka kuwa machungu ya mavunjiko, nao mlima wa Nyumba ya Bwana utakuwa kilima chenye mwitu. Je? Hizikiya, mfalme wa Yuda, nao Wayuda wote walimwua? Hakumcha Bwana na kuutuliza uso wake Bwana? Naye Bwana akageuza moyo, asiwafanyizie hayo mabaya, aliyowaambia. Na sisi tufanye kibaya kilicho kikuu kama hicho, tuzikoseshe roho zetu? Kulikuwa na mtu mwingine aliyefumbua katika Jina la Bwana, ni Uria, mwana wa Semaya wa mji wa Kiriati-Yearimu. Naye akayafumbua yote yatakayoujia mji huu na nchi hii sawasawa kama Yeremia. Mfalme Yoyakimu na watu wake wote wa vita na wakuu wote walipoyasikia maneno yake, mfalme akatafuta, jinsi atakavyomwua. Uria alipoyasikia, akaogopa, akakimbia kwenda Misri. Mfalme Yoyakimu akatuma watu kwenda Misri; ni Elnatani, mwana wa Akibori, na watu wengine waliokwenda naye Misri. Wakamtoa Uria huko Misri, wakampeleka kwake mfalme Yoyakimu, akampiga kwa upanga, mzoga wake akautupa kwenye makaburi yao waliokuwa wa ukoo huu. Lakini Ahikamu, mwana wa Safani, alimshika Yeremia kwa mkono wake, asitiwe mikononi mwa watu wamwue. Katika mwanzo wa ufalme wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia likitoka kwake Bwana kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Jitengenezee kamba na kongwa, uzitie shingoni pako! Kisha uzitume kwa mfalme wa Edomu na kwa mfalme wa Moabu na kwa Mfalme wa wana wa Amoni na kwa mfalme wa Tiro na kwa mfalme wa Sidoni, ukizitia mikononi mwa wajumbe wanaokuja Yerusalemu kwa Sedekia, mfalme wa Yuda! Uwaagize, wawaambie mabwana wao kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema, navyo ndivyo, mtakavyowaambia mabwana wenu: Mimi nilizifanya nchi na watu na nyama wa porini walioko katika nchi kwa nguvu yangu iliyo kuu na kwa mkono wangu uliokunjuka, nikampa anyokaye machoni pangu. Sasa mimi nimezitia nchi hizi zote mkononi mwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, aliye mtumishi wangu; hata nyama wa porini nimempa, wamtumikie. Mataifa yote yatamtumikia yeye na mwanawe na mjukuu wake, mpaka zitakapotimia siku za nchi yake; ndipo, mataifa yenye watu wengi na wafalme wakuu watakapomtumikisha naye. Itakuwa, taifa au ufalme utakaokataa kumtumikia Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, na kuzitia shingo zao katika makongwa ya mfalme wa Babeli, watu wa taifa hilo nitawapatiliza kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya. Kwa hiyo ninyi msiwasikie wafumbuaji wenu wala waaguaji wenu wala ndoto zenu wala waganga wenu wala watazamaji wenu wanaowaambia kwamba: Hamtamtumikia mfalme wa Babeli! Kwani huwafumbulia yenye uwongo, kusudi wawatoe katika nchi yenu na kuwapeleka katika nchi ya mbali, nami niwatupe ninyi, mwangamie. Lakini watu wa taifa litakalotia shingo zao katika makongwa ya mfalme wa Babeli, wamtumikie, nitawatuliza katika nchi yao, wailime wakikaa kwao; ndivyo, asemavyo Bwana. Kisha nikamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno haya yote ya kwamba: Zitieni shingo zenu katika makongwa ya mfalme wa Babeli, mmtumikie yeye na watu wake wote, mpate kukaa! Kwa sababu gani mnataka kufa, wewe nao walio ukoo wako, kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya, kama Bwana alivyosema kwa ajili ya taifa litakalokataa kumtumikia mfalme wa Babeli? Msiyasikie maneno ya wafumbuaji wanaowaambia kwamba: Msimtumikie mfalme wa Babeli! Kwani hao huwafumbulia yenye uwongo. Ndivyo, asemavyo Bwana: Sikuwatuma, nao hufumbua katika Jina langu yenye uwongo, kusudi niwatupe ninyi, mwangamie ninyi na wafumbuaji waliowafumbulia ninyi. Nao watambikaji na watu wote wa ukoo huu nikawaambia kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msiyasikie maneno ya wafumbuaji wenu wanaowafumbulia kwamba: Mtaona, vyombo vya Nyumba ya Bwana vikirudishwa toka Babeli sasa bado kidogo tu! Kwani hao huwafumbulia yenye uwongo. Msiwasikie! Ila mtumikieni mfalme wa Babeli, mpate kukaa! Kwa nini mji huu ugeuke kuwa mavunjiko? Kama ndio wafumbuaji, kama Neno la Bwana liko kwao, na wamwombe Bwana Mwenye vikosi, vyombo vilivyosalia katika Nyumba ya Bwana namo nyumbani mwa mfalme wa Yuda namo Yerusalemu visiende Babeli! Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema kwa ajili yao: Zile nguzo na bahari na vilingo na vyombo vyote vilivyosalia humu mjini, kweli Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, hakuvichukua alipomhamisha Yekonia, mwana wa Yoyakimu, mfalme wa Yuda, toka Yerusalemu kwenda Babeli pamoja na wakuu wote wa Yuda na wa Yerusalemu; lakini hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema kwa ajili ya vyombo vilivyosalia Nyumbani mwa Bwana namo nyumbani mwa mfalme wa Yuda namo Yerusalemu: Vitapelekwa Babeli; ndiko, vitakakokuwa mpaka siku ile, nitakapowapatiliza; ndivyo, asemavyo Bwana. Ndipo, mtakapovileta huku na kuvirudisha mahali hapa. Ikawa mwaka uleule, ufalme wa Sedekia, mfalme wa Yuda, ulipoanzia, katika mwezi wa tano wa mwaka wa nne, ndipo, mfumbuaji Hanania, mwana wa Azuri wa Gibeoni, aliponiambia Nyumbani mwa Bwana machoni pao watambikaji napo pao wote wa ukoo huu kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema kwamba: Nimeyavunja makongwa ya mfalme wa Babeli. Bado miaka miwili ndipo, mimi nitakapovirudisha mahali hapa vyombo vyote vya Nyumba ya Bwana, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alivyovichukua mahali hapa na kuvipeleka Babeli. Naye Yekonia, mwana wa Yoyakimu, mfalme wa Yuda, nayo mateka yote ya Yuda waliokwenda Babeli mimi nitawarudisha mahali hapa, kwani nitayavunja makongwa ya mfalme wa Babeli; ndivyo, asemavyo Bwana. Mfumbuaji Yeremia akamwambia mfumbuaji Hanania machoni pao watambikaji napo pao watu wote wa ukoo huu waliosimama katika Nyumba ya Bwana, akasema mfumbuaji Yeremia: Amin, na yawe hivyo! Bwana na ayafanye hivyo akiyatimiza maneno yako, uliyoyafumbua, akivirudisha mahali hapa vyombo vya Nyumba ya Bwana nayo mateka yote toka Babeli! Lisikie tu neno hili, ninalolisema masikioni mwako, namo masikioni mwa watu wote wa ukoo huu: Wafumbuaji waliokuwa mbele yangu na mbele yako toka siku za kale walifumbulia nchi nyingi, hata nchi zenye wafalme wakuu vita na mabaya na magonjwa yauayo yatakayokuja. Lakini mfumbuaji anayefumbua mambo ya kutuliza roho atajulikana hapo, lile neno lake mfumbuaji litakapotimia, ya kuwa ni mfumbuaji, Bwana aliyemtuma kweli. Ndipo, mfumbuaji Hanania alipoiondoa miti ya kongwa shingoni pake Yeremia, akaivunja. Kisha Hanania akasema, watu wote wa ukoo huu wakimtazama, kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Hivi ndivyo, nitakavyoyavunja makongwa ya Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, shingoni pa mataifa yote, miaka miwili itakapopita. Kisha mfumbuaji Yeremia akashika njia kwenda zake. Neno la Bwana likamjia Yeremia, mfumbuaji Hanania alipokwisha kuivunja miti ya kongwa shingoni pake mfumbuaji Yeremia, likamwambia: Nenda kumwambia Hanania haya: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Miti ya kongwa, uliyoivunja, ni ya miti tu; lakini mahali pao umeweka miti ya kongwa iliyo ya chuma. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Makongwa ya chuma nimetia shingoni pao haya mataifa yote, wamtumikie Nebukadinesari, mfalme wa Babeli; watamtumikia kweli, nao nyama wa porini nimempa. Basi, mfumbuaji Yeremia akamwambia mfumbuaji Hanania: Sikia, Hanania! Bwana hakukutuma, nawe umewaegemeza watu wa ukoo huu mambo ya uwongo. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kweli: Utaniona, nikikutuma kuondoka huku nchini, mwaka huu wewe utakufa, kwani umewakataza watu kumtii Bwana. Mfumbuaji Hanania akafa mwaka uleule katika mwezi wa saba. Haya ndiyo maneno ya barua ya mfumbuaji Yeremia, aliyoiandika Yerusalemu kwenda kwao wazee waliosalia kwao waliotekwa na kwa watambikaji na kwa wafumbuaji na kwa watu wote wa ukoo huu, Nebukadinesari aliowateka Yerusalemu na kuwapeleka Babeli. Mfalme Yekonia na mama yake walipokwisha kutoka Yerusalemu pamoja na wakuu wa nyumba ya mfalme na wakuu wa Yuda na wa Yerusalemu na mafundi wa seremala na wahunzi, ndipo, alipoitia mikononi mwao Elasa, mwana wa Safani, na Gemaria, mwana wa Hilkia; hawa ndio, Sedekia, mfalme wa Yuda, aliowatuma kwenda Babeli kwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli. Akawaandikia: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyowaambia mateka yote, niliowatoa Yerusalemu, wapelekwe Babeli: Jengeni nyumba, mkae! Limeni mashamba, mle mazao yao! Oeni wanawake, mzae watoto wa kiume na wa kike! Nao wana wenu wa kiume wapatieni wanawake, nao wana wenu wa kike mwaoze waume, wazae watoto wa kiume na wa kike, mwe wengi huko, msipunguke! Utafuteni utengemano wa ule mji, niliowahamishia ninyi! Uombeeni kwa Bwana! Kwani unapotengemana, nanyi mtapata kutengemana. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Wasiwadanganye wafumbuaji walioko kwenu katikati wala waaguaji wenu! Wala msizisikie ndoto zenu, mnazoziota! Kwani hao huwafumbulia maneno yenye uwongo katika Jina langu, sikuwatuma; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwanza sharti miaka 70 ipite huko Babeli; ndipo, nitakapowatokea, niwatimizie lile neno langu jema la kwamba: Nitawarudisha mahali hapa. Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Mimi ninayajua mawazo, ninayowawazia, kuwa mawazo ya kuwaponya, siyo ya kuwaponza, nipate kuwapa huko nyuma myangojeayo. Mtakaponiita mkiendelea kunilalamikia, nitawasikia. Mtakaponitafuta, mtaniona; mtakaponitafuta kwa mioyo yote, nitawaonekea, nitawafungua mafungo yenu, niwakusanye na kuwatoa kwenye mataifa yote na mahali po pote, nilipowahamishia; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani ninyi husema: Bwana ametuinulia wafumbuaji huku Babeli. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya mfalme anayekaa katika kiti cha kifalme cha Dawidi na kwa ajili ya watu wote wa ukoo huu wanaokaa humu mjini walio ndugu zenu, wasiotoka pamoja nanyi kwenda kuhamishwa; hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Wataniona, nikituma kwao panga na njaa na magonjwa mabaya, nikiwageuza kuwa kuyu zitapishazo, zisizolika kwa ubaya wao. Nitawakimbiza kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya, nitawatoa, watupwe huko na huko katika nchi zote zenye wafalme huku ulimwenguni, waapizwe kwa kustukiwa, wazomelewe na kutukanwa kwenye mataifa yote, nitakakowatupa, kwa kuwa hawakuyasikia maneno yangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Mimi nilituma kwao watumishi wangu walio wafumbuaji pasipo kuchoka kila kulipokucha, lakini hamkusikia; ndivyo, asemavyo Bwana. Lakini ninyi lisikieni Neno la Bwana, ninyi mateka yote, niliowatoa Yerusalemu na kuwatuma kwenda Babeli! Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema kwa ajili ya Ahabu, mwana wa Kolaya, na kwa ajili ya Sedekia, mwana wa Masea, waliowafumbulia katika Jina langu mambo ya uwongo: Mtaniona, nikiwatia mkononi mwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, awaue machoni penu. Nako kwao ndiko, mateka yote ya Wayuda walioko Babeli watakakochukua kiapo cha kwamba: Bwana na akufanyizie kama Ahabu na kama Sedekia, mfalme wa Babeli aliowachoma motoni! Kwa kuwa wamefanya yasiyofanywa kwao Waisiraeli, wakifanya ugoni na wanawake wa wenzao, wakasema neno la uwongo katika Jina langu, nami sikuwaagiza neno, Mimi ninayajua haya, ninayashuhudia. Kwa ajili ya Semaya wa Nehelamu utasema kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema kwamba: Umetuma barua katika jina lako kwa watu wote wa ukoo huu waliomo Yerusalemu na kwa mtambikaji Sefania, mwana wa Masea, na kwa Yerusalemu na kwa watambikaji wote, za kwamba: Bwana amekuweka kuwa mtambikaji mahali pa mtambikaji Yoyada, mwe wasimamizi Nyumbani mwa Bwana kuwaangalia wote wenye wazimu nao wajiwaziao kuwa wafumbuaji, uwafunge mikatale na mapingu. Mbona sasa hukumkaripia Yeremia wa Anatoti anayewafumbulia ninyi? Kwa sababu hii ametuma kwetu Babeli barua ya kwamba: Siku ni nyingi bado, jengeni nyumba, mkae! Limeni mashamba, mle mazao yao! Mtambikaji Sefania alipoisoma barua hii masikioni pa mfumbuaji Yeremia, ndipo, neno la Bwana lilipomjia Yeremia kwamba: Tuma barua kwa mateka yote kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya Semaya wa Nehelamu: Kwa kuwa Semaya amewafumbulia ninyi, nami sikumtuma, akawaegemeza mambo ya uwongo, kwa hiyo Bwana anasema haya: Mtaniona, nikimpatiliza Semaya wa Nehelamu na kizazi chake: hatapata mtu wa mlango wake atakayekaa kwao wa ukoo huu, wala atakayeyaona yale mema, nitakayowafanyizia wao walio ukoo wangu, kwani amewakataza watu kumtii Bwana; ndivyo, asemavyo Bwana. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema kwamba: Yaandike hayo maneno yote, niliyokuambia katika kitabu! Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Tazama! Siku zitakuja, nitakapoyafungua mafungo yao walio ukoo wangu wa Isiraeli na wa Yuda, niwarudishe katika ile nchi, niliyowapa baba zao, nayo itakuwa yao tena; ndivyo, Bwana anavyosema. Haya ndiyo maneno, Bwana aliyoyasema kwa ajili ya Isiraeli na ya Yuda, kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tumesikia sauti ya kustusha na kushangaza, hakuna penye utengemano. Ulizeni, mwone, kama yuko mwanamume atakayezaa! Mbona nimewaona waume wote wakitia mikono yao viunoni pao kama mwanamke anayetaka kuzaa? Mbona nyuso zote zimegeuka, zikachujuka? Kumbe siku hiyo ni kubwa, hakuna ifananayo nayo; ndipo, Yakobo anaposongeka, lakini napo atapatoka, aokoke. Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Itakuwa siku ile, nitakapoyavunja makongwa shingoni pako na kuyararua mafungo yako, wageni wasiwatumikishe tena. Ila watamtumikia Bwana Mungu wao na Dawidi, mfalme wao, nitakayemwinua kwao. Ndivyo, asemavyo Bwana: Nawe, mtumishi wangu Yakobo, usiogope, wala usistuke, Isiraeli! Kwani utaniona, nikikuokoa na kukutoa katika nchi za mbali, nacho kizazi chako nitakitoa katika nchi, walikofungiwa. Yakobo atarudi, atatulia pasipo kusumbuliwa, kwani hakuna atakayemhangaisha. Kwani mimi niko pamoja na wewe nikuokoe; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani nitayamaliza mataifa yote, ambayo nimekutawanya kwao, wewe peke yako sitakumaliza, nitakuchapa tu, kama yakupasavyo, nisikuache pasipo patilizo lo lote. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kidonda chako hakiwezekani, pigo lako haliponi. Hakuna akupigiaye shauri, alitoe jipu lako usaha; hakuna dawa ya kubandika, ikuponye. Wote waliokupenda wamekusahau, hawakuulizi tena, kwani nimekupiga, kama ninavyopiga mchukivu, nimekuchapa pasipo huruma, kwa kuwa ulifanya maovu mengi, kweli makosa yako ni makali. Mbona unakililia kidonda chako, ya kuwa maumivu yako hayawezekani? Nimekufanyizia hayo, kwa kuwa ulifanya maovu mengi, nayo makosa yako ni makali. Kweli wote waliokula wewe wataliwa, nao wote waliokusonga watakwenda kufungwa; waliokunyang'anya nao watanyang'anywa, nao wote waliopokonya mali zako nitawatoa, wapokonywe nao mali zao. Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Nitakupatia uzima tena, hata vidonda vyako nitaviponya, kwa kuwa wewe Sioni wamekuita Mfukuzwa kwa kwamba: Hakuna anayemwuliza. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikiyafungua mafungo ya mahema yake Yakobo, nikiyahurumia makao yake; nao mji utajengwa tena juu ya chungu zake, hata jumba kuu litakaa, kama yalipasavyo. Namo mwao zitatoka nyimbo za kushukuru na sauti zao wachekao; nami nitawapa kuwa wengi, wasiwe wachache, nitawapa utukufu, wasibezwe. Nao watoto wao watakuwa kama kale; nalo kundi lao la watu litapata nguvu usoni pangu, nao wote waliowakorofisha nitawapatiliza. Mkuu wao atakuwa mtu wa kwao; atakayewatawala atatoka katikati yao; nami nitamfikisha, anijie karibu, kwani yuko nani ajipaye moyo wa kunijia mwenyewe? ndivyo, asemavyo Bwana. Nanyi mtakuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Mtakiona kimbunga cha Bwana, hata makaa yenye moto yakitoka kwake, nao upepo wa chamchela wenye nguvu utawaangukia vichwani wao wasiomcha Mungu. Ukali wake Bwana wenye moto hautatulia, mpaka uyafanye na kuyatimiza mawazo ya moyo wake; siku za mwisho mtayatambua haya. Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku zile nitaiwia milango yote ya Isiraeli Mungu wao, nao wataniwia ukoo wangu. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: ukoo wao waliosazwa na panga wameona upole nyikani, kwa kuwa watakwenda kwenye pumzikio la Bwana. Bwana amenionekea toka mbali akiniambia: Nimekupenda kwa upendo wa kale na kale, kwa hiyo nimekuvuta kwa kukuhurumia, uje kwangu. Nitakujenga; ndipo, utakapokuwa umejengwa, wewe mwanamwali wa Isiraeli! Utajipamba tena na kupiga patu, utatoka nao wachezao ngoma wakicheka. Utapanda tena mizabibu katika milima ya Samaria, nao wapanzi walioipanda wataichuma. Kwani iko siku, walinzi watakapoita mlimani kwa Efuraimu kwamba: Inukeni, tupande kwenda Sioni kwa Bwana Mungu wetu! Kwani, hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mpigieni Yakobo vigelegele vya furaha! Mwimbieni sana aliye kichwa chao mataifa! Pazeni sauti na kumshangilia! Semeni: Bwana, waokoe, walio ukoo wako, walio masao ya Waisiraeli! Mtaniona, nikiwaleta na kuwatoa katika nchi ya upande wa kaskazini, nikiwakusanya na kuwatoa mapeoni kwa nchi, nao vipofu na viwete, hata wenye mimba pamoja nao wazaao, watakuwa kundi kubwa, watakaporudi huku. Watakuja na kulia, nami nitawaongoza, wakinilalamikia; nitawapeleka kwenye vijito vya maji na kushika njia inyokayo, wasijikwae hapo, kwani nitakuwa baba yao Waisiraeli, nao Waefuraimu watakuwa kama mwanangu wa kwanza. Lisikieni Neno la Bwana, ninyi mataifa! Litangazeni kwenye visiwa vilivyoko mbali! Semeni: Aliyewatawanya Waisiraeli anawakusanya na kuwalinda, kama mchungaji anavyolilinda kundi lake. Kwani Bwana amewaokoa walio wa Yakobo, akawaokoa mikononi mwake aliyewashinda nguvu. Watakuja, wapige vigelegele mlimani kwa Sioni na kuyakimbilia mema ya Bwana, ngano na mvinyo na mafuta na wana wa kondoo na ndama; ndipo, roho zao zitakapokuwa kama shamba lenye maji, hawatazimia tena kwa njaa. Ndipo, wanawali watakapofurahia tena kucheza ngoma pamoja na vijana wa kiume na wazee pia, kwani ndipo, nitakapoyageuza masikitiko yao, yawe machangamko, nikiwatuliza mioyo na kuwafurahisha, wayaache majonzi yao. Hata roho zao watambikaji nitazipendeza na kuwapa manono, nao walio ukoo wangu watashiba mema; ndivyo, asemavyo Bwana. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Sauti imesikiwa Rama, ni kilio na maombolezo yenye uchungu. Raheli anawalilia watoto wake, hakutaka kubembelezwa kwa ajili ya watoto wake, kwani hawako. Lakini hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ukataze umio wako, usilie! Nayo macho yako yakataze, yasitoe machozi! Kwani mshahara wa matendo yako uko, hao watarudi wakitoka katika nchi ya adui; ndivyo, asemavyo Bwana. Tena kiko kingojeo kitakachotimia siku zilizoko mbele yako, kwani wanao watarudi kwenye mipaka yao; ndivyo, asemavyo Bwana. Nimemsikia Efuraimu, akipiga kilio kwamba: Umeniponda, nikapondeka kama ndama asiyefundishwa bado; nigeuze! ndipo, nitakapokuwa nimegeuka. Kwani wewe ndiwe Bwana Mungu wangu. Kwani nilipokuwa nimegeuka, nilijuta; nilipokuwa nimeonyeka, nilijipiga kiuno, nikaona soni na kuiva uso, kwani nilikuwa nimetwishwa matusi ya ujana wangu. Je? Efuraimu siye mwanangu mwenye kiasi kikuu? Siye mtoto wa kupendezwa naye? Ijapo nimemtisha, ninamkumbuka tena, nao moyo wangu unajihangaisha kwa ajili yake, mpaka nimhurumie; ndivyo, asemavyo Bwana. Jisimamishie yaonyeshayo njia, kajiwekee vielekezo, nazo njia, ulizozipita ulipokwenda, zitie moyoni mwako! Rudini, mlio wanawali wa Isiraeli! Rudini katika hii miji yenu! Mnataka kutangatanga mpaka lini, ninyi wasichana wakatavu! Kwani Bwana ataumba jambo lililo jipya katika nchi: mwanamke atamkingia mumewe! Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Nitakapoyafungua mafungo yao, watu watalitumia tena neno hilo katika nchi ya Yuda namo mijini mwao la kwamba: Bwana na akubariki, uliye mbuga yenye wongofu, uliye mlima wenye utakatifu! Nao Wayuda watakaa huku katika miji yao yote iliyoko, walio wakulima nao watembeao na makundi. Kwani roho zilizozimia kwa kiu nitazirudisha na kuzinywesha, nazo roho zilizozimia kwa njaa nitazishibisha. Kisha nikaamka, nikaona, ya kuwa hivyo, nilivyolala usingizi, vimenipendeza sana. Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, nitakapoumwagia mlango wa Isiraeli na mlango wa Yuda mbegu za watu na mbegu za nyama. Itakuwa, kama nilivyokuwa macho na kuangalia, wang'olewe, wapondwe, wavunjwe, waangamizwe, wafanyiziwe mabaya, ndivyo, nitakavyokuwa macho na kuangalia, wajengwe, wapandwe; ndivyo, asemavyo Bwana. Siku zile hawatasema tena: Baba walipokula zabibu bichi, ndipo, wana walipokufa ganzi la meno. Ila kila mtu atauawa na manza, alizozikora yeye; hata kila mtu atakayekula zabibu bichi atakufa mwenyewe ganzi la meno. *Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, nitakapofanya nao wa mlango wa Isiraeli nao wa mlango wa Yuda Agano Jipya. Halitakuwa, kama Agano lile lilivyokuwa, nililolifanya na baba zao siku ile, nilipowashika mikono, niwatoe katika nchi ya Misri; lile Agano langu walilivunja, kama mimi si Bwana wao; ndivyo, asemavyo Bwana. Agano, nitakalolifanya nao wa mlango wa Isiraeli, siku hizi zitakapokuwa zimepita, ni hili: Nitawapa Maonyo yangu, yakae katika mawazo yao, tena nitayaandika mioyoni mwao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Hawatafundishana tena mtu na mwenziwe, wala mtu na ndugu yake kwamba: Mjueni Bwana! Kwani wote watanijua, hivyo walivyo wadogo, mpaka wakiwa wakubwa, kwani nitawaondolea manza zao, walizozikora, nisiyakumbuke tena makosa yao; ndivyo, asemavyo Bwana.* Hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliyeliweka jua kuwa mwanga wa mchana hata miandamo ya mwezi pamoja na nyota kuwa mwanga wa usiku; ni yeye anayeichafua bahari, mawimbi yake yavume. Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake; basi, ndivyo, asemavyo Bwana: Hapo, matengenezo hayo yatakapotoweka machoni pangu, ndipo, walio wa kizazi cha Isiraeli watakapokoma, wasiwe taifa la siku zote machoni pangu. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Hapo, mbingu zilizoko juu zitakapopimika, hapo, misingi ya nchi itakapochunguzika, ndipo, nitakapowatupa wote walio wa kizazi cha Isiraeli kwa ajili ya matendo yao yote; ndivyo, asemavyo Bwana. Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, mji huu utakapojengwa kuwa wa Bwana kuanzia kwenye mnara wa Hananeli kulifikisha lango la pembeni; toka hapo kamba ya kupimia itakwenda tena moja kwa moja mpaka kwenye kilima cha Garebu, hapo itazunguka kwenda Goa. Nalo bonde lote la mizoga na la majivu na mashamba yote mpaka kwenye mto wa Kidoroni na mpaka pembeni kwa Lango la Farasi lililoko upande wa maawioni kwa jua yatakuwa Patakatifu pa Bwana, hapatang'olewa tena, wala hapatavunjwa tena kale na kale. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwake Bwana katika mwaka wa 10 wa Sedekia, mfalme wa Yuda, ndio mwaka wa 18 wa Nebukadinesari. Ilikuwa hapo, vikosi vya mfalme wa Babeli vilipousonga Yerusalemu; naye mfumbuaji Yeremia alikuwa amefungwa uani penye kifungo kilichokuwa kwenye nyumba ya mfalme wa Yuda. Aliyemfunga ni Sedekia, mfalme wa Yuda, kwa kwamba: Mbona unafumbua kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikiutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, auteke. Naye Sedekia, mfalme wa Yuda, hatapona mikononi mwa Wakasidi, kwani atatiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli, watasemeana kinywa kwa kinywa wakionana macho kwa macho. Atampeleka Sedekia Babeli; ndiko, atakakokuwa, mpaka nitakapomkagua; ndivyo, asemavyo Bwana: Mtakapopigana na Wakasidi hamtafanikiwa. Yeremia akasema: Neno la Bwana limenijia kwamba: Utamwona Hanameli, mwana wa mjomba wako Salumu, akija kwako kukuambia: Jinunulie shamba langu lililoko Anatoti! Kwani wewe unapaswa na kulikomboa, liwe lako. Kisha Hanameli, mwana wa mjomba wangu, akaja kwangu uani penye kifungo, kama Bwana alivyoniambia, akaniambia: Jinunulie shamba langu lililoko Anatoti katika nchi ya Benyamini, kwani inakupasa wewe kuwa nalo kwa kulikomboa. Nikatambua; ya kuwa hili ni lile neno la Bwana. Nikalinunua lile shamba kwake Hanameli, mwana wa mjomba wangu, lililoko Anatoti, nikamlipa fedha, nazo zilikuwa fedha kumi na saba. Nikaliandika katika cheti, nikatia muhuri, kikashuhudiwa na mashahidi, kisha nikampa fedha zake na kuzipima katika mizani. Nikakichukua kile cheti cha ununuzi chenye muhuri kilichoandikwa maagano na maongozi, tena kingine kilicho wazi. Hicho cheti cha ununuzi nikampa Baruku, mwana wa Neria, mwana wa Masea, machoni pake Hanameli, mwana wa mjomba wangu, napo machoni pao mashahidi walioyaandika majina yao katika cheti cha ununuzi napo machoni pao Wayuda wote waliokaa uani penye kifungo. Nikamwagiza Baruku machoni pao hivyo: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Vichukue vyeti hivi, cheti cha ununuzi chenye muhuri nacho cheti hiki kilicho wazi, uvitie katika chombo cha udongo, vipate kukaa siku nyingi. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Nyumba na mashamba na mizabibu itanunuliwa tena katika nchi hii. Nilipokuwa nimekwisha kumpa Baruku, mwana wa Neria, cheti cha ununuzi nikamwomba Bwana kwamba: E Bwana Mungu, tazama, wewe ulizifanya mbingu na nchi kwa uwezo wako mkubwa na kwa mkono wako ukunjukao, hakuna kisichowezekana kwako. Watu maelfu huwahurumia, nazo manza, baba walizozikora, huzilipiza kwa wana wao waliotokea nyuma yao. U Mungu mkuu mwenye nguvu; Bwana Mwenye vikosi ni Jina lako. Mashauri yako ni makuu, matendo yako ni mengi, macho yako hufumbuka, yazione njia zote za wana wa watu, umpe kila mtu yazipasayo njia zake nayo yayapasayo mapato ya matendo yake. Ulifanya vielekezo na vioja katika nchi ya Misri mpaka siku hii ya leo kwa Waisiraeli hata kwa watu wengine, ukajipatia Jina, kama linavyojulikana leo. Walio ukoo wako wa Isiraeli ukawatoa katika nchi ya Misri kwa kufanya vielekezo na vioja kwa kiganja chenye nguvu cha mkono ukunjukao, ukatisha kwa matisho makuu. Ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kuwapa, ni nchi ichuruzikayo asali na maziwa. Wakaja, wakaitwaa, kisha hawakuisikia sauti yako, wala hawakuyafuata Maonyo yako, wala hawakuyafanya yote, uliyowaagiza, wayafanye; kwa hiyo umewaletea haya mabaya yote. Tunayaona haya maboma, yako karibu, ni ya kuutekea mji huu; kweli mji huu utatiwa mikononi mwa Wakasidi wanaoupigia vita, maana panga na njaa na magonjwa mabaya yataushinda, yatimie uliyoyasema, nawe utakuwa ukiyatazama tu. Wewe Bwana Mungu, umeniambia: Jinunulie shamba kwa fedha, mashahidi wakiwako kuvishuhudia. Lakini mji huu utatiwa mikononi mwa Wakasidi. Neno la Bwana likamjia Yeremia kwamba: Tazama! Mimi ni Bwana, Mungu wao wote walio wenye miili. Je? Liko lo lote lisilowezekana kwangu? Kwa hiyo Bwana anasema hivi: Mtaniona kweli, nikiutia mji huu mikononi mwao Wakasidi namo mkononi mwake Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, auteke. Kweli Wakasidi wanaoupigia mji huu vita watauingia, watauchoma moto mji huu na kuziteketeza nyumba, walimomvukizia Baali darini juu, nazo zile, walimomwagia miungu mingine vinywaji vya tambiko, kusudi wanikasirishe. Kwani wana wa Isiraeli nao wana wa Yuda tangu ujana wao huyafanya yale tu yaliyokuwa mabaya machoni pangu, kweli wana wa Isiraeli wamenikasirisha kwa matendo ya mikono yao; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani mji huu umenichafua na kuuwakisha moto wa makali yangu kuanzia siku ile, walipoujenga mpaka siku hii ya leo; kwa hiyo ninauondoa usoni pangu kwa ajili ya mabaya yote, wana wa Isiraeli na wana wa Yuda waliyoyafanya, kusudi wanikasirishe, wao wenyewe na wafalme wao na wakuu wao na watambikaji wao na wafumbuaji wao, walio watu wa Yuda nao wakaao Yerusalemu. Wakanigeuzia kosi zao, sizo nyuso; nami naliwafundisha pasipo kuchoka kila kulipokucha, lakini hawakuwako waliosikia, waonyeke. Wakayaweka matapisho yao katika ile Nyumba iliyoitwa kwa Jina langu, waitie uchafu. Wakamjengea Baali pa kumtambikia vilimani juu katika Bonde la Mwana wa Hinomu, wawatumie wana wao wa kiume na wa kike kuwa ng'ombe za tambiko za Moloki, nami sikuwaagiza hivyo, wala havikunijia moyoni, ya kuwa watafanya tapisho kama hilo, kusudi wawakoseshe Wayuda. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema sasa kwa ajili ya mji huu, ambao mnasema, ya kuwa umetiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli kwa nguvu za panga na za njaa na za magonjwa mabaya: Mtaniona, nikiwakusanya na kuwatoa katika nchi zote, nilikowaendesha na kuwakimbiza kwa makali yangu yaliyowaka moto na kwa machafuko makuu, nitawarudisha mahali hapa na kuwapa kukaa salama. Nao watakuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Nami nitawapa kuwa wenye moyo mmoja washikao njia moja tu, waniogope siku zao zote; hivyo watajipatia mema wenyewe hata wana wao watakaokuwa nyuma yao. Nitafanya nao agano la kale na kale, ya kuwa sitaacha kuwafuata na kuwafanyizia mema, namo mioyoni mwao nitatia woga wa kuniogopa, wasiondoke tena kwangu. Nami nitawafurahia, niwafanyizie mema, kweli nitawapanda katika nchi hii kwa moyo wangu wote na kwa roho yangu yote. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kama nilivyowaletea wao wa ukoo huu haya mabaya yote yaliyo makuu, ndivyo, nitakavyowaletea mema yote, niliyowaambia mimi. Mashamba yatanunuliwa tena katika nchi hii, mnayoisema ninyi, ya kuwa ni nyika tu pasipo watu na nyama kwa kutiwa mikononi mwa Wakasidi. Mashamba yatanunuliwa kwa fedha, hata vyeti vya ununuzi vitaandikwa na kutiwa muhuri na kushuhudiwa na mashahidi katika nchi ya Benyamini na pande zote za Yerusalemu, namo katika miji ya Yuda, namo katika miji iliyoko milimani, namo katika miji iliyoko mbugani, namo katika miji iliyoko upande wa kusini; kwani nitayafungua mafungo yao; ndivyo, asemavyo Bwana. Neno la Bwana likamjia Yeremia mara ya pili, alipokuwa amefungwa bado uani penye kifungo, la kwamba: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliye mwenye kuvifanya, anavyovitengeneza, avitimize, Bwana ni Jina lake. Niite! ndipo, nitakapokujibu, nikuambie mambo makuu yaliyo magumu, usiyoyajua. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema kwa ajili ya nyumba za mji huu na kwa ajili ya nyumba za wafalme wa Yuda zilizobomolewa, zitumike kujenga maboma ya kuzuilia panga; akasema hata kwa ajili yao waliokuja kupigana na Wakasidi, lakini wakawapatia tu watu wengi wa kuwaua, ndio wao, niliowapiga kwa makali yangu yaliyowaka moto, ndio wao, niliowaficha uso wangu, watu wa mji huu wasiuone kwa ajili ya mabaya yao. Mtaniona, nikiwapatia uzima na uponya; nitawaponya, kisha nitawafunulia mfuriko wa utengemano ulio wa kweli. Nitayafungua mafungo ya Wayuda na mafungo ya Waisiraeli, nitawajenga, wawe, kama walivyokuwa mwanzo. Nitawaeua, maovu yote, waliyonikosea, yawatoke, nikiwaondolea hayo maovu yao yote, waliyonikosea na kunitengua. Ndipo, jina lake huo mji litakapokuwa la kunifurahisha kwa kunisifu na kunitukuza kwenye mataifa yote ya huku nchini, kwani watayasikia mema yote, mimi niliyowafanyizia, nao watastuka na kutetemeka kwa ajili ya hayo mema yote na kwa ajili ya huo utengemano wote, nitakaowapatia mimi. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ninyi mnapaita mahali hapa Penye mavunjiko, kwa kuwa hapana mtu wala nyama, lakini hapa napo penye miji ya Yuda na penye barabara za Yerusalemu zilizo peke yao, kwa kuwa hapana mtu wala apitaye wala akaaye wala hapana nyama, ndipo, patakaposikilika tena sauti za vicheko na sauti za furaha, hata sauti za wachumba wa kiume na wa kike, tena sauti zao wasemao: Mshukuruni Bwana Mwenye vikosi, ya kuwa Bwana ni mwema! Ya kuwa upole wake ni wa kale na kale! Watavileta vipaji vyao vya kumshukuru katika Nyumba ya Bwana, kwani nitayafungua mafungo ya nchi hii, iwe, kama ilivyokuwa mwanzo. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mahali hapa palipo Penye mavunjiko, kwa kuwa hapana mtu wala nyama, napo penye miji yake yote patakuwa tena na malisho ya wachungaji, wanapowapumzisha kondoo wao. Katika miji iliyoko milimani, namo katika miji iliyoko mbugani, namo katika miji iliyoko upande wa kusini, hata katika nchi ya Benyamini na pande zote za Yerusalemu, namo katika miji ya Yuda makundi ya kondoo yatapita tena yakichungwa na mikono yao wanaowahesabu; ndivyo, Bwana anavyosema. Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, nitakapolitimiza lile neno jema, nililowaambia walio wa mlango wa Isiraeli nao walio wa mlango wa Yuda! Siku zile za wakati ule zitakapotimia, ndipo, nitakapomchipuzia Dawidi chipuko lenye wongofu, naye atafanya katika nchi hii yaliyo sawa yaongokayo. Siku zile ndipo, nchi ya Yuda itakapookolewa, nao mji wa Yerusalemu utakaa salama, nalo jina, utakaloitwa ni hili: Bwana ni wongofu wetu. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwao wa Dawidi hatakoseka mtu atakayekaa katika kiti cha kifalme cha mlango wa Isiraeli. Hata kwao watambikaji na Walawi hatakoseka mtu wa kutumikia usoni pangu, kama ni kuteketeza ng'ombe za tambiko au kuvukiza vipaji vya tambiko au kuyatengeneza matoleo ya tambiko ya kila siku. Neno la Bwana likamjia Yeremia kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Hamwezi kulivunja agano langu la mchana wala agano langu la usiku, pasiwe mchana wala usiku panapopasa. Vilevile agano langu, nililoliagana na mtumishi wangu Dawidi, halitawezekana kuvunjwa asiwe na mwanawe atakayetawala na kukaa katika kiti chake cha kifalme, wala wasipatikane Walawi walio watambikaji wa kunitumikia. Kama vikosi vya mbinguni visivyohesabika, tena kama mchanga wa baharini usivyopimika, ndivyo, nitakavyowafurikisha walio wa kizazi cha mtumishi wangu Dawidi kuwa wengi, hata Walawi wanaonitumikia. Neno la Bwana likamjia Yeremia kwamba: Hukusikia, watu hawa wa huku wanavyosema kwamba: Koo mbili, Bwana alizozichagua, amezitupa? Kwa hiyo huwabeza walio ukoo wangu, wasiwe taifa tena machoni pao. Lakini hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Agano langu la mchana na la usiku liko, nayo maongozi ya mbinguni na ya nchini yako, hayaondoki. Vilevile sitawatupa walio wa kizazi cha Yakobo na cha Dawidi, wala sitaacha kuchukua katika kizazi chake watakaowatawala walio wa kizazi cha Aburahamu na cha Isaka na cha Yakobo, kwani nitayafungua mafungo yao nitakapowahurumia. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, na vikosi vyake vyote na watu wa nchi zote za kifalme, mkono wake ulizozitawala, hayo makabila yote walipopiga vita, wauteke Yerusalemu na miji yake yote, likawa la kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Nenda kumwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, ukimwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Utaniona, nikiutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, auteketeze kwa moto! Nawe hutaopoka mkononi mwake, kwani utakamatwa, utiwe mkononi mwake, nawe utaonana na mfalme wa Babeli macho kwa macho, atasema na wewe kinywa kwa kinywa, nawe utakwenda Babeli. Lisikie tu neno lake Bwana, wewe Sedekia, mfalme wa Yuda! Haya ndiyo, Bwana anayokuambia: Utakufa na kutulia; kama baba zako waliokuwa wafalme wa kwanza, waliokuwa mbele yako, walivyowashiwa mioto, ndivyo, watakavyokuwashia nawe mioto wakikuombolezea kwamba: E Bwana! Kwani hili ndilo neno, nililolisema mimi; ndivyo, asemavyo Bwana. Mfumbuaji Yeremia akamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno haya yote mle Yerusalemu, vikosi vya mfalme wa Babeli walipoupigia Yerusalemu vita, wauteke pamoja na miji yote ya Yuda iliyosalia, ndiyo Lakisi na Azeka; kwani hiyo ndiyo iliyosalia katika miji ya Yuda iliyokuwa yenye maboma. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana hapo, mfalme Sedekia alipokwisha kuagana na watu wote waliokuwamo Yerusalemu kuwatangazia watumwa ukombozi, kila mtu amwachilie mtumwa wake na kijakazi wake walio wa Kiebureo, akiwapa ruhusa, wajiendee tu, tena mtu asimtumikishe tena mwenziwe kazi za kutumwa katika nchi ya Yuda. Wakayasikia wakuu wote nao watu wote walioingia katika agano hilo la kwamba: Kila mtu ampe mtumwa wake na kijakazi wake ruhusa, wajiendee tu, asiwatumikishe tena kazi za kitumwa; nao walipoyasikia, wakawapa ruhusa, wajiendee tu. Lakini walipokwisha kufanya hivyo wakawarudia, wakawarudisha watumwa na vijakazi, waliowapa ruhusa, wajiendee tu, wakawashurutisha tena kuwa watumwa na vijakazi. Kwa hiyo neno la Bwana likamjia Yeremia likitoka kwa Bwana kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mimi nilifanya Agano na baba zenu siku ile, nilipowatoa katika nchi ya Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa, kwamba: Mwisho wa miaka saba, kila mtu akiwa na ndugu yake wa Kiebureo aliyenunuliwa nawe, sharti umpe ruhusa, atoke kwako, ajiendee tu. Akutumikie miaka sita, kisha sharti umpe ruhusa, atoke kwako, ajiendee tu! Lakini baba zenu hawakunisikia, wala hawakuyatega masikio yao. Nanyi mmefanya leo tena yanyokayo machoni pangu, kila mtu akimtangazia mwenziwe ukombozi, mkaagana hivyo usoni pangu katika Nyumba hii inayoitwa kwa Jina langu. Lakini mkawarudia, mkalitia Jina langu uchafu mkiwarudisha kila mtu mtumwa wake na kijakazi wake, mliowapa ruhusa, wajiendee roho zao zilikotaka, mkawashurutisha kuwa tena watumwa na vijakazi wenu. Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Hamkunisikia mkimtangazia kila mtu ndugu yake na mwenzake ukombozi. Kwa hiyo ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona nikiwatangazia ukombozi na kuwaitia panga na magonjwa mabaya na njaa, nitawatoa ninyi, mtupwe huko na huko katika nchi zote zenye wafalme huku nchini. Nao waume waliolivunja agano wasipoyatimiza maneno ya hilo agano, walilolifanya usoni pangu, nitawatoa kuwa kama ndama ya tambiko, waliyoikata vipande viwili, kisha huipitia katikati. Wakuu wa nchi ya Yuda nao wakuu wa Yerusalemu nao wakuu wa nyumba za mfalme nao watambikaji nao watu wote wa nchi hii waliovipitia vipande vya ndama ya tambiko katikati, hao wote nitawatia mikononi mwa adui zao namo mikononi mwao wanaozitafuta roho zao, nayo mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani na cha nyama wa porini. Naye Sedekia, mfalme wa Yuda, nao wakuu wake nitawatia mikononi mwao adui zao namo mikononi mwao wanaozitafuta roho zao namo mikononi mwa vikosi vya mfalme wa Babeli, vilivyotoka kwenu kwenda zao. Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona nikiwaagiza na kuwarudisha penye mji huu, waupigie vita, wauteke, wauteketeze kwa moto; nayo miji ya Yuda nitaitoa kuwa mapori tu, pasikae mtu. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana siku za Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, kwamba: Nenda nyumbani mwao Warekabu kusema nao, uwapeleke Nyumbani mwa Bwana katika ukumbi mmoja, uwape mvinyo, wanywe. Nikamchukua Yazania, mwana wa Yeremia, mwana wa Habasinia, pamoja na ndugu zake na wanawe wote nao wote walio wa mlango wa Warekabu. Nikawapeleka Nyumbani mwa Bwana katika ukumbi wa wana wa Hanani, mwana wa Igidalia, aliyekuwa mtu wa Mungu. Nao ukumbi huo ulikuwa kando ya ukumbi wa wakuu uliokuwa juu ya ukumbi wa Masea, mwana wa Salumu, aliyekuwa mlinda kizingiti. Kisha nikaweka mbele yao walio wa mlango wa Warekabu mitungi iliyojaa mvinyo na vikombe, nikawaambia: Nyweni mvinyo! Wakajibu: Hatunywi mvinyo, kwani Yonadabu, mwana wa baba yetu Rekabu, alituagiza kwamba: Msinywe mvinyo ninyi na wana wenu kale na kale! Wala msijenge nyumba, wala msimwage mbegu, wala msipande mizabibu, wala msiwe nayo! Ila mkae mahemani siku zenu zote, mpate kuwapo siku nyingi huku nchini, mliko wageni ninyi. Tukaisikia sauti ya Yonadabu, mwana wa baba yetu Rekabu, katika mambo yote, aliyotuagiza, tusinywe mvinyo sisi wala wake zetu wala wana wetu wa kiume na wa kike: hatujengi nyumba za kukaa humo, wala mizabibu wala mashamba wala mbegu hatunazo. Tunakaa mahemani, kwani tumeyasikia, tukayafanya yote, kama baba yetu Yonadabu alivyotuagiza. Ikawa, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alipopanda katika nchi hii, ndipo, tuliposema: Haya! Na tuje kwenda Yerusalemu na kuvikimbia vikosi vya Wakasidi na vya Washami! Basi, tukakaa Yerusalemu. Neno la Bwana likamjia Yeremia kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Nenda kuwaambia watu wa Yuda nao wakaao Yerusalemu: Je? Hamtaki kuonyeka, myasikie maneno yangu? Ndivyo, asemavyo Bwana: Maneno yake Yonadabu, mwana wa Rekabu, aliyowaagiza wanawe, wasinywe mvinyo, yametimizwa nao: hawanywi mvinyo hata siku hii ya leo, kwani wamelisikia agizo la baba yao. Mimi nami nimesema nanyi pasipo kuchoka kila kulipokucha, lakini hamkunisikia. Nikatuma kwenu watumishi wangu wote walio wafumbuaji pasipo kuchoka kila kulipokucha kwamba: Rudini kila mtu katika njia yake mbaya na kufanya matendo mema! Msifuate miungu mingine kuitumikia! Ndipo, mtakaporudi katika nchi, niliyowapa baba zenu! Lakini hamkuyatega masikio yenu, wala hamkunisikia. Kweli, wana wa Yonadabu, mwana wa Rekabu, wamelitimiza agizo la baba yao, alilowaagiza; lakini wao wa ukoo huu hawanisikii. Kweli, hivi ndivyo, Bwana Mungu Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaona, nikiwaletea Wayuda nao wakaao Yerusalemu yale mabaya yote, niliyoyasema ya kuwafanyizia, kwa kuwa niliposema nao, hawakunisikia, nilipowaita, hawakujibu. Nao walio wa mlango wa Rekabu Yeremia akawaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Kwa kuwa mmelisikia agizo la baba yenu Yonadabu, mkayashika maagizo yake yote, mkayafanya yote, kama alivyowaagiza, kwa hiyo ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Hatakoseka mtu wa Yonadabu, mwana wa Rekabu, atakayesimama usoni pangu siku zote. Ikawa katika mwaka wa 4 wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, ndipo, neno hili lilipomjia Yeremia likitoka kwa Bwana kwamba: Jichukulie kitabu cha kuzingwa, uandike humo maneno yote niliyokuambia kwa ajili ya Isiraeli na ya Yuda na ya mataifa yote, anzia siku ile, niliposema na wewe, tangu siku za Yosia mpaka siku hii ya leo. Labda watasikia walio wa mlango wa Yuda wakiambiwa mabaya yote, mimi ninayoyawaza kuwafanyizia, kusudi warudi kila mtu katika njia yake mbaya, nikiwaondolea manza zao na makosa yao. Yeremia akamwita Baruku, mwana wa Neria; kisha Baruku akayaandika katika kitabu cha kuzingwa maneno yote ya Bwana, aliyomwambia, kama Yeremia alivyoyasema kwa kinywa chake. Yeremia akamwagiza Baruku kwamba: Mimi nimefungwa, siwezi kwenda Nyumbani mwa Bwana. Kwa hiyo nenda, ukisome hiki kitabu, ulichokiandika maneno ya Bwana, kama nilivyoyasema kwa kinywa changu, watu wayasikie Nyumbani mwa Bwana siku ya kufunga mfungo, hata Wayuda wote waliokuja wakitoka mijini mwao sharti wayasikie, yakisomwa. Labda malalamiko yao yatamwangukia Bwana usoni pake, wakirudi kila mtu katika njia zake mbaya, kwani makali yenye moto ni makuu, Bwana aliyoyasema kuwafanyizia watu wa ukoo huu. Baruku, mwana wa Neria, akayafanya yote, kama mfumbuaji Yeremia alivyomwagiza, akayasoma mle kitabuni maneno ya Bwana Nyumbani mwake Bwana. Ikawa katika mwaka wa 5 wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa tisa, ndipo, walipotangaza, watu wote wa Yerusalemu nao watu wote waliotoka katika miji ya Yuda kuja Yerusalemu wamfungie Bwana. Baruku akayasoma mle kitabuni maneno ya Yeremia Nyumbani mwa Bwana katika ukumbi wa Gemaria, mwana wa Safani, aliyekuwa mwandishi penye ua wa juu kwenye lango jipya la Nyumba ya Bwana, watu wote wa ukoo huu wakayasikia. Naye Mikaya, mwana wa Gemaria, mwana wa Safani, akayasikia maneno yote ya Bwana, yaliposomwa mle kitabuni. Akashuka kwenda nyumbani mwa mfalme katika ukumbi wa mwandishi, akawakuta humo wakuu wote, wakikaa, akina mwandishi Elisama na Delaya, mwana wa Semaya, na Elnatani, mwana wa Akibori, na Gemaria, mwana wa Safani, na Sedekia, mwana wa Hanania, nao wakuu wote. Basi, Mikaya akawasimulia hayo maneno yote, aliyoyasikia, Baruku aliyoyasoma mle kitabuni masikioni pao wa ukoo huu. Ndipo, wakuu wote walipomtuma Yudi, mwana wa Netania, mwana wa Selemia, mwana wa Kusi, kwenda kwake Baruku kumwambia: Kitabu cha kuzingwa, ulichokisoma masikioni pao wa ukoo huu, kichukue mkononi mwako, uje huku! Baruku, mwana wa Neria, akakichukua kile kitabu cha kuzingwa mkononi mwake, akaja kwao. Wakamwambia: Kaa, ukisome napo masikioni petu! Baruku akakisoma masikioni pao. Walipoyasikia haya maneno yote, ndipo, walipostukiana kila mtu na mwenziwe, wakamwambia Baruku: Sharti tumjulishe mfalme maneno haya yote! Wakamwambia Baruku kwamba: Tusimulie, jinsi ulivyoyaandika maneno haya yote, kinywa chake kilipoyasema! Baruku akawaambia: Kwa kinywa chake akanisomea maneno haya yote, nami nikayaandika humu kitabuni kwa wino. Kisha wakuu wakamwambia Baruku: Nenda kujificha wewe na Yeremia, mtu asijue, mliko ninyi! Nao wakaja kwa mfalme uani kwake, lakini kile kitabu cha kuzingwa walikuwa wamekiweka vizuri katika ukumbi wa mwandishi Elisama, wakayasimulia hayo maneno yote masikioni pa mfalme. Mfalme akamtuma Yudi kukichukua kile kitabu cha kuzingwa, akakichukua hicho kitabu katika ukumbi wa mwandishi Elisama, Yudi akakisoma masikioni pake mfalme napo masikioni pao wakuu wote waliosimama na kumzunguka mfalme. Naye mfalme akakaa katika nyumba ya kipupwe kwa kuwa mwezi wa tisa, nacho chano chenye makaa kikawaka moto mbele yake. Ikawa, Yudi alipokwisha kusoma vipindi vitatu au vinne, mfalme akavikata kwa kisu cha mwandishi, akavitupa motoni penye chano, mpaka alipokwisha kukitupa kitabu kile cha kuzingwa chote motoni penye chano. Hawakustuka wala hawakuzirarua nguo zao, wala mfalme wala watumishi wake wote walioyasikia maneno hayo yote. Napo hapo, Elnatani na Delaya na Gemaria walipomwomba mfalme sanasana, asikiteketeze hicho kitabu cha kuzingwa, hakuwasikia. Mfalme akamwagiza Yerameli, mwana wa mfalme, na Seraya, mwana wa Azirieli, na Selemia, mwana wa Abudeli, kumchukua mwandishi Baruku na mfumbuaji Yeremia, lakini Bwana aliwaficha. Neno la Bwana likamjia Yeremia, mfalme alipokwisha kukiteketeza kile kitabu cha kuzingwa na maneno yote, Baruku aliyoyaandika humo kwa kuambiwa na kinywa chake, likamwambia: Jichukulie tena kitabu cha kuzingwa, ukiandike maneno hayo yote ya kwanza yaliyokuwamo katika kitabu kile cha kuzingwa cha kwanza, Yoyakimu, mfalme wa Yuda, alichokiteketeza. Lakini kwa ajili ya Yoyakimu, mfalme wa Yuda, utasema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Wewe umekiteketeza kitabu hicho cha kuzingwa kwamba: Mbona umeandika humo kwamba: Mfalme wa Babeli atakuja kweli kuiharibu nchi hii na kukomesha huku watu na nyama? Kwa hiyo Bwana anasema hivi kwa ajili ya Yoyakimu, mfalme wa Yuda: Hatampata atakayekaa katika kiti cha kifalme cha Dawidi, nao mzoga wake utakuwa umetupiwa jua kali la mchana nayo baridi ya usiku. Nitampatilizia yeye na kizazi chake na watumishi wake manza zao, walizozikora, nikiwaletea wao nao wakaao Yerusalemu nao watu wa Yuda mabaya yote, niliyoyasema, ya kuwa nitawafanyizia, lakini hawakusikia. Ndipo, Yeremia alipochukua kitabu kingine cha kuzingwa, akampa mwandishi Baruku, mwana wa Neria, akayaandika humo, Yeremia aliyoyasema kwa kinywa chake, ni maneno yote ya kile kitabu, Yoyakimu, mfalme wa Yuda, alichokiteketeza kwa moto, pakaongezwa tena maneno mengi kama hayo. Sedekia, mwana wa Yosia, akawa mfalme mahali pake Konia, mwana wa Yoyakimu, aliyemweka Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, kuwa mfalme wa Yuda. Yeye na watumishi wake na watu wa nchi yake hawakuyasikia maneno ya Bwana, aliyoyasema kwa kumtumia mfumbuaji Yeremia. Mfalme Sedekia akamtuma Yukali, mwana wa Selemia, na Sefania, mwana wa mtambikaji Masea, kwenda kwa Yeremia kumwambia: Tuombee kwake Bwana Mungu wetu! Kwani Yeremia alikuwa akiingia, tena akitoka kwa watu, hawakumfunga katika nyumba ya kifungo. Ndipo, vikosi vya Farao vilipotoka Misri; Wakasidi waliousonga Yerusalemu walipousikia uvumi wao, wakaondoka hapo Yerusalemu. Neno la Bwana likamjia mfumbuaji Yeremia kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Haya ndiyo, mmwambie mfalme wa Yuda aliyewatuma kwangu kuniuliza: Tazama! Vikosi vya Farao vilivyotoka kwao kuja kuwasaidia wamekwisha kurudi katika nchi yao ya Misri. Lakini Wakasidi watarudi, waupigie mji huu vita; nao watauteka na kuuteketeza kwa moto. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msijidanganye wenyewe na kusema: Wakasidi wataondoka kwetu kwenda zao! Kwani hawatakwenda. Kwani kama mngevipiga vikosi vyote vya Wakasidi wanaopigana nanyi, wakasalia kwao watu wenye vidonda tu, wangeinuka kila mtu katika hema lake, wauteketeze mji huu kwa moto. Ikawa, vikosi vya Wakasidi vilipoondoka Yerusalemu kwa kuvikimbia vikosi vya Farao, ndipo, Yeremia naye alipotoka Yerusalemu kwenda katika nchi ya Benyamini, alichukue fungu lake lililoko kule kwa watu wa huko katikati. Alipofika penye lango la Benyamini, kulikuwako mkuu wa walinzi, jina lake Iria, mwana wa Selemia, mwana wa Hanania, akamkamata mfumbuaji Yeremia kwamba: Utawaangukia Wakasidi wewe! Yeremia akajibu: Ni uwongo! Mimi siwaangukii Wakasidi, lakini hakumsikia; ndipo, Iria alipomkamata Yeremia na kumpeleka kwa wakuu. Wakuu wakamtolea Yeremia ukali, wakampiga; kisha wakamtia kifungoni nyumbani mwa mwandishi Yonatani, kwani walikuwa wakiitumia kuwa nyumba ya kifungo. Hivi ndivyo, Yeremia alivyoingia katika ile nyumba yenye mashimo yaliyochimbuliwa upande wa ndani chini; ndimo, Yeremia alimokaa siku nyingi. Kisha mfalme Sedekia akatuma kumchukua; mfalme akamwuliza nyumbani mwake penye njama kwamba: Liko neno lililotoka kwa Bwana? Yeremia akasema: Liko; kisha akamwambia: Utatiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli. Yeremia akamwuliza mfalme Sedekia: Nimekukosea nini au watumishi wako au watu wa ukoo huu, mkinitia kifungoni? Wako wapi wafumbuaji wenu waliowafumbulia kwamba: Mfalme wa Babeli hatafika kwenu wala katika nchi hii? Sasa sikiliza, bwana wangu mfalme, nayo malalamiko yangu na yakuangukie usoni: Usinirudishe nyumbani mwa Yonatani, nisife mle! Mfalme Sedekia alipotoa amri, wakamfunga Yeremia tena uani penye kifungo, akapewa kila siku mkate wa ngano uliotoka huko, wachoma mikate wanakokaa, mpaka mikate ilipotoweka mjini. Ndivyo, Yeremia alivyopata kukaa uani penye kifungo. Sefatia, mwana wa Matani, na Gedalia, mwana wa Pashuri, na Yukali, mwana wa Selemia, na Pashuri, mwana wa Malkia, wakayasikia yale maneno, Yeremia aliyowaambia watu wote wa ukoo huu kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Akaaye humu mjini atakufa kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya; lakini atakayewatokea Wakasidi atapona, roho yake itakuwa pato lake. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mji huu utatiwa kweli mikononi mwao vikosi vya mfalme wa Babeli, atauteka. Wakuu wakamwambia mfalme: Mtu huyu sharti auawe! Kwani anailegeza mikono ya wapiga vita waliosalia humu mjini, nayo mikono yao wote walio wa ukoo huu, akiwaambia maneno kama hayo; kwani mtu huyu hatafuti, jinsi watu watakavyokaa salama, ila jinsi watakavyoona mabaya. Mfalme Sedekia akawaambia: Tazameni! Yumo mikononi mwenu. Kwani hakuna mfalme awashindaye ninyi jambo lo lote. Wakamchukua Yeremia, wakamtupa katika kisima cha Malkia, mwana wa mfalme, kilichokuwa hapo uani penye kifungo, wakamshusha Yeremia mle kwa kamba. Mle kisimani hamkuwa na maji, ila ni matopetope tu, Yeremia akaanza kuzama matopeni. Mnubi Ebedimeleki aliyekuwa mtumishi nyumbani mwa mfalme akasikia, ya kuwa wamemtumbukiza Yeremia mle kisimani. Siku moja, mfalme alipokaa penye lango la Benyamini, Ebedimeleki akatoka nyumbani mwa mfalme, akaja kusema na mfalme kwamba: Bwana wangu mfalme, yote, watu waliyomfanyizia mfumbuaji Yeremia, ni mabaya, wakimtupa kisimani, afie mle ndani kwa njaa, kwani hamna mkate tena humu mjini. Ndipo, mfalme alipomwagiza yule Mnubi Ebedimeleki kwamba: Chukua hapa kwa mkono wako watu thelathini, umwopoe mfumbuaji Yeremia mle kisimani, angaliko hajafa bado! Ebedimeleki akawachukua wale watu kwa mkono wake, akaingia nyumbani mwa mfalme chumba cha chini cha kuwekea malimbiko, akachukua mle vitambaa vya nguo zilizopasuka na vitambaa vya nguo chakavu, akavishusha kwa kamba kisimani kwake Yeremia. Yule Mnubi Ebedimeleki akamwambia Yeremia: Hivi vitambaa vya nguo zipasukazo na vya nguo chakavu vitie makwapani chini ya kamba! Yeremia akayafanya hivyo. Kisha wakamvuta Yeremia kwa hizo kamba, wakamwopoa kisimani, Yeremia akakaa tena uani penye kifungo. Mfalme Sedekia akatuma kumchukua mfumbuaji Yeremia, aje kwake penye lango la tatu la kuiingilia Nyumba ya Bwana, mfalme akamwambia Yeremia: Mimi ninataka kukuuliza neno, lakini usinifiche lo lote! Yeremia akamwambia Sedekia: Je? Nikikujulisha yote, hutaniua? Tena nikikupa shauri, hutanisikia. Ndipo, mfalme alipomwapia Yeremia penye njama kwamba: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, aliyetuumbia hii roho yetu, sitakuua, wala sitakutia mikononi mwao watu hawa wanaoitafuta roho yako. Ndipo, Yeremia alipomwambia Sedekia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Kama utawatokea wakuu wa mfalme wa Babeli, roho yako itapona, nao mji huu hautateketezwa kwa moto; hivyo utapona wewe na mlango wako. Lakini usipowatokea wakuu wa mfalme wa Babeli, mji huu utatiwa mikononi mwao Wakasidi, wauteketeze kwa moto, wewe nawe hutapona mikononi mwao. Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia: Mimi ninawaogopa Wayuda waliorudi upande wa Wakasidi, wasinitie mikononi mwao, nao wakanizomea. Yeremia akamjibu: Hawatakutoa. Isikie tu sauti ya Bwana, niliyokuambia mimi! Ndivyo, utakavyoona mema, nayo roho yako itapona. Lakini wewe ukikataa kuwatokea, basi, neno, Bwana alilonionyesha, ni hili: Utaona, wanawake wote waliosalia nyumbani mwa mfalme wa Yuda wakitolewa na kupelekwa kwa wakuu wa mfalme wa Babeli; nao watakwenda wakisema: Wamekupoteza, wakakushinda wale, uliotengemana nao! Lakini hapo, miguu yako iliposhikwa na matope, wamerudi nyuma! Wakeo wote na wanao wa kiume wote watawatoa na kuwapeleka kwa Wakasidi, wewe nawe hutapona mikononi mwao, kwani utakamatwa kwa mikono ya mfalme wa Babeli, nao mji huu utateketea kwa moto. Ndipo, Sedekia alipomwambia Yeremia: Mtu ye yote asiyajue haya maneno, wewe usife! Kama wakuu wanasikia, ya kuwa nimesema na wewe, wakija kwako kukuambia: Tusimulie, uliyomwambia mfalme, usitufiche! Hatutakuua, tusimulie nayo, mfalme aliyokuambia! ndipo, utakapowaambia: Mimi nimekuwa nikimlalamikia mfalme na kumwangukia, asinirudishe nyumbani mwa Yonatani, nisifie mle! Wakuu wakaja kwake Yeremia, wakamwuliza, akawaambia hayo maneno yote, kama mfalme alivyomwagiza, wakamwacha na kunyamaza, kwani lile shauri halikujulikana. Kisha Yeremia akakaa uani penye kifungo mpaka siku ile, Yerusalemu ulipotekwa. Yerusalemu ukatekwa hivyo: katika mwaka wa 9 wa Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa 9 Nebukadinesari, mfalme wa Babeli alikuja Yerusalemu na vikosi vyake vyote, wakaanza kuusonga. Katika mwaka wa 11 wa Sedekia katika mwezi wa nne siku ya tisa boma la mji likabomolewa. Wakaingia wakuu wote wa mfalme wa Babeli, wakakaa penye lango la kati, ni Nergali-Sareseri na Samugari-Nebu na Sarsikimu, mkuu wa watumishi wa nyumbani mwa mfalme, na Nergali-Sareseri, mkuu wa waaguaji, nao wengine wote waliokuwa wakuu wa mfalme wa Babeli. Sedekia, mfalme wa Yuda, alipowaona yeye na wapiga vita wote, ndipo, walipokimbia, wakatoka mjini na usiku kwa njia ya bustani ya mfalme wakipita lango lililokuwa katikati ya zile kuta mbili za boma, wakaishika njia ya kwenda nyikani. Vikosi vya Wakasidi vikawafuata na kupiga mbio, wakamfikia Sedekia katika nyika ya Yeriko, wakamkamata, wakampeleka kwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, mjini mwa Ribula katika nchi ya Hamati, yeye akasema naye na kumhukumu. Mfalme wa Babeli akawaua wana wa Sedekia machoni pake yeye huko Ribula, nao wakuu wote wa Yuda mfalme wa Babeli akawaua. Kisha akayapofua macho ya Sedekia, akamfunga kwa minyororo, ampeleke Babeli. Nyumba ya mfalme na nyumba za watu Wakasidi wakaziteketeza kwa moto, nazo kuta za boma la Yerusalemu wakazibomoa. Lakini masao ya watu wa ukoo huu, waliosalia mjini, ndio waliokuwa wamerudi upande wao na kuwaangukia nayo masao mengine ya watu waliosalia wakatekwa, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawapeleka Babeli. Lakini waliokuwa wanyonge wa ukoo huu, wasiokuwa na kitu, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawaacha katika nchi ya Yuda, akawapa mashamba ya mizabibu na mashamba mengine siku ile. Nebukadinesari mfalme wa Babeli, akamtia Yeremia mkononi mwa Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akimwagiza kwamba: Mchukue, mwangalie kwa macho yako, usimfanyizie kibaya cho chote, ila mwenyewe atakavyokuambia, basi, ndivyo umfanyizie! Ndipo, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, na Nebusazibani, mkuu wa watumishi wa nyumbani mwa mfalme, na Nergali-Sareseri, mkuu wa waaguaji, nao wakuu wote wa mfalme wa Babeli walipotuma, wakamchukua Yeremia wakimtoa uani penye kifungo, wakamwagiza Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Safani, amtoe kifungoni na kumpa ruhusa kwenda nyumbani, akakaa katikati ya watu. Neno la Bwana lilimjia Yeremia, alipokuwa amefungwa uani penye kifungo, kwamba: Nenda kumwambia Ebedimeleki, yule Mnubi, kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Utaniona, nikiuletea mji huu niliyoyasema, yauwie, nayo ni mabaya, siyo mema, yatatimia usoni pako siku ile. Lakini ndivyo, asemavyo Bwana: Wewe nitakuponya siku hiyo, hutatiwa mikononi mwao watu wale, unaowaogopa. Kwani nitakuponya, usiuawe kwa upanga, nayo roho yako itakuwa pato lako, kwani umenitegemea; ndivyo, asemavyo Bwana. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, alipompa ruhusa huko Rama kujiendea; naye alimpata, alipokuwa amefungwa kwa minyororo, katikati ya mateka yote ya Yerusalemu na ya Yuda waliokwenda kupelekwa Babeli. Hapo, mkuu wao waliomlinda mfalme alipomchukua Yeremia, akamwambia: Bwana Mungu wako aliyasema haya mabaya, ya kuwa yatapajia mahali hapa. Basi, ameyaleta, akayafanya, kama alivyoyasema, kwani mmemkosea Bwana, msipoisikia sauti yake; ndipo, jambo hili lilipofanyika kwenu. Sasa tazama! Nimekufungulia leo minyororo, mikono yako iliyofungwa nayo; vikiwa vema machoni pako kwenda na mimi kufika Babeli, njoo! nitakuangalia kwa macho yangu. Lakini vikiwa vibaya machoni pako kwenda na mimi kufika Babeli, acha! Tazama, nchi hii yote iko mbele yako, patakapokuwa pema kwa kufaa machoni pako, nenda pale! Alipokuwa hajaenda bado huko wala huko, akamwambia: Rudi kwake Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Safani, mfalme wa Babeli aliyemweka kuwa msimamizi katika miji ya Yuda, ukae naye katikati yao walio wa ukoo wako! Au po pote palipofaa machoni pako kwenda kukaa, nenda hapo! Kisha mkuu wao waliomlinda mfalme akampa pamba za njiani na matunzo, akampa ruhusa kujiendea. Yeremia akaja Misipa kwake Gedalia, mwana wa Ahikamu, akakaa naye katikati yao walio wa ukoo wake, waliosazwa katika nchi hiyo. Wakuu wote wa vikosi waliokuwa bado porini na watu wao waliposikia, ya kuwa mfalme wa Babeli amemweka Gedalia, mwana wa Ahikamu, kuisimamia nchi hiyo, akimpa waume na wake na watoto nao wanyonge wa nchi hiyo nao wasiopelekwa Babeli, ndipo, walipokuja Misipa kwa Gedalia. Ndio Isimaeli, mwana wa Netania, na Yohana na Yonatani, wana wa Karea, na Seraya, mwana wa Tanumeti, nao wana wa Efe wa Netofa na Yezania, mwana wa mtu wa Maka, hao wenyewe na watu wao. Waume hawa na watu wao Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana Safani, akawaapia kwamba: Msiogope kuwatumikia Wakasidi! Kaeni katika nchi hii na kumtumikia mfalme wa Babeli! ndipo, mtakapoona mema. Nami mnaniona: ninakaa Misipa, nisimame mbele yao Wakasidi, watakaokuja kwetu. Nanyi mtachuma zabibu na matunda mengine ya kiangazi nayo yaliyo yenye mafuta, myaweke katika vyombo vyenu mkikaa katika miji yenu, mtakayoichukua. Nao Wayuda wote waliokuwako Moabu kwa wana wa Amoni na Edomu na katika nchi zote waliposikia, ya kuwa mfalme wa Babeli ameacha masao katika nchi ya Yuda, akamweka Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Safani, kuwaangalia, ndipo, waliporudi Wayuda wote wakitoka mahali po pote, walipotupiwa, wakaja Misipa katika nchi ya Yuda kwa Gedalia, wakachuma zabibu na matunda ya kiangazi mengi sana. Yohana, mwana wa Karea, nao wakuu wote wa vikosi waliokuwa porini bado walipokuja Misipa kwa Gedalia, wakamwambia: Unajua, ya kuwa Balisi, mfalme wa wana wa Amoni, amemtuma Isimaeli, mwana wa Netania, akuue wewe? Lakini Gedalia, mwana wa Ahikamu, hakuwategemea. Ndipo, Yohana, mwana wa Karea, alipomwambia Gedalia penye njama huko Misipa kwamba: Na niende, nimwue Isimaeli, mwana wa Netania, mtu asijue! Kwa nini akuue wewe mwenyewe, Wayuda wote waliokusanyika kwako watawanyike tena, hayo masao ya Yuda yaangamie? Lakini Gedalia, mwana wa Ahikamu, akamwambia Yohana, mwana wa Karea: Usilifanye neno hili! Kwani unamsemea Isimaeli uwongo. Ikawa katika mwezi wa saba, ndipo, Isimaeli, mwana wa Netania, mwana wa Elisama wa kizazi cha kifalme, aliyekuwa mkuu wa mfalme, alipokuja Misipa pamoja na watu kumi kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, wakala chakula pamoja naye huko Misipa. Ndipo, Isimaeli, mwana wa Netania, alipoinuka na wale watu kumi waliokuwa naye, wakampiga Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Safani, kwa panga, mpaka wakamwua; naye ndiye, mfalme wa Babeli aliyemweka kuisimamia nchi hiyo. Nao Wayuda wote waliokuwa Misipa pamoja na Gedalia, nao Wakasidi waliopatikana kule, nao wapiga vita Isimaeli akawaua. Ikawa, hata siku ya pili ya kumwua Gedalia mtu hakuvijua. Wakaja watu waliotoka Sikemu na Silo na Samaria, nao walikuwa watu 80 waliojinyoa ndevu na kuvaa nguo zilizoraruliwa, tena walikuwa wamejikatakata chale, namo mikononi mwao walichukua vipaji vya tambiko na uvumba kuvipeleka Nyumbani mwa Bwana. Isimaeli, mwana wa Netania akatoka Misipa, akawaendea, akienda akilia machozi; alipowafikia akawaambia: Njoni kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu! Ikawa, walipofika mjini kati, ndipo, Isimaeli, mwana wa Netania, alipowaua, akawatumbukiza kisimani, yeye na watu waliokuwa naye. Kwao wale kukaonekana watu kumi, wakamwambia Isimaeli: Usituue! Kwani tuko na vilimbiko, tulivyovificha porini, vya ngano na vya mawele na vya mafuta na vya asali; ndipo, alipowaacha, asiwaue pamoja na ndugu zao. Hicho kisima, Isimaeli alimoitumbukizia mizoga yao yote, aliowaua, walipokuja kwa Gedalia, ni kile, mfalme Asa alichokifanya kwa ajili ya kupigana na Basa, mfalme wa Isiraeli; hicho ndicho, Isimaeli, mwana wa Netania, alichokijaza mizoga yao, aliowaua. Kisha Isimaeli akawateka watu wote wa ukoo huu waliosalia Misipa: wana wa kike wa mfalme nao wote pia walioachwa Misipa, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, aliompa Gedalia, mwana wa Ahikamu, awaangalie. Basi, Isimaeli, mwana wa Netania, akawateka, akashika njia kwenda kujitia kwa wana wa Amoni. Yohana, mwana wa Karea, nao wakuu wote wa vikosi waliokuwa naye walipoyasikia hayo mabaya yote Isimaeli, mwana wa Netania, aliyoyafanya, wakawachukua watu wote, wakaenda kupigana na Isimaeli, mwana wa Netania, wakamwona penye maji mengi karibu ya Gibeoni. Ikawa, watu wote wa ukoo huu waliokuwa na Isimaeli walipomwona Yohana, mwana wa Karea, nao wakuu wote wa vikosi waliokuwa naye, wakafurahi. Ndipo, watu wote wa ukoo huu, Isimaeli aliowateka Misipa, wakageuka nyuma, wakarudi kwenda kwa Yohana, mwana wa Karea. Isimaeli, mwana wa Netania, akamkimbia Yohana pamoja na watu wanane, akaenda kwa wana wa Amoni. Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa vikosi waliokuwa naye wakawachukua watu wote wa ukoo huu waliosalia, wakawarudisha na kuwatoa kwa Isimaeli, mwana wa Netania, aliowateka Misipa, alipokwisha kumwua Gedalia, mwana wa Ahikamu, nao walikuwa waume wapigao vita na wanawake na watoto na watumishi wa mfalme wa nyumbani, basi, wakawarudisha toka Gibeoni. Wakaondoka, wakakaa penye fikio la Kimuhamu lililoko kando ya Beti-Lehemu, wakataka kwenda Misri, kwa kuwakimbia Wakasidi, kwani waliwaogopa, kwa kuwa Isimaeli, mwana wa Netania, alimwua Gedalia, mwana wa Ahikamu, mfalme wa Babeli aliyemweka kuisimamia nchi hiyo. Wakuu wote wa vikosi na Yohana, mwana wa Karea, na Yezania, mwana wa Hosaya, nao watu wote wa ukoo huu, wadogo kwa wakubwa, wakamjia mfumbuaji Yeremia, wakamwambia: Malalamiko yetu na yakuangukie, utuombee kwa Bwana Mungu wako sisi sote tuliosazwa huku! Kwani tumesalia wachache tu kwa wale wengi, kama macho yako yanavyotuona sisi. Bwana Mungu wako atuonyeshe njia, tutakayoishika, na jambo, tutakalolifanya. Mfumbuaji Yeremia akawaambia: Nimesikia; sasa hivi nitawaombea kwa Bwana Mungu wenu kwa ajili ya njia yenu; kila neno, Bwana atakalowajibu, nitawaambia, sitawanyima neno kamwe. Nao wakamwambia Yeremia: Bwana na awe kwetu shahidi mkweli na mtegemevu kwamba: Kila neno, Bwana Mungu wako atakalokutuma, litakavyotuambia, ndivyo, tutakavyofanya. Kama ni jema au kama ni baya, sauti ya Bwana Mungu wetu tutaisikia, kwa kuwa tunakutuma kwake, kusudi tuone mema tukiisikia sauti ya Bwana Mungu wetu. Siku kumi zilipopita, neno la Bwana likamjia Yeremia, akamwita Yohana, mwana wa Karea, nao wakuu wote wa vikosi waliokuwa naye, nao watu wote wa ukoo huu, wadogo kwa wakubwa, akawaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema, kwa kuwa mmenituma kwake, kumpelekea malalamiko yenu, yamwangukie, akasema: Mtakapokaa tu katika nchi hii, nitawajenga, nisiwabomoe tena, nitawapanda, nisiwang'oe tena, kwani nitageuza moyo, nisiyafanye yale mabaya, niliyowawazia. Msimwogope mfalme wa Babeli, mnayemwogopa ninyi! Ndivyo, asemavyo Bwana: Msimwogope, kwani mimi niko pamoja nanyi, niwaokoe na kuwaponya mikononi mwake! Nami nitawapatia huruma, awahurumie na kuwarudisha katika nchi yenu. Lakini ninyi mkisema: Hatutakaa katika nchi hii, msiisikie sauti ya Bwana Mungu wenu; mkisema: Hivi sivyo, sharti tuende Misri, maana hatutaona huko vita, wala sauti za mabaragumu hazitasikilika huko, wala hatutaona njaa kwa kukosa chakula, kwa hiyo tunataka kukaa huko; basi, sasa lisikieni neno la Bwana, ninyi mlio masao ya Yuda: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Kama mnazielekeza nyuso zenu kwenda Misri, mkaja kukaa ugenini huko, ndipo, panga, ninyi mnazoziogopa, zitakapowafikia katika nchi ya Misri, nayo njaa inayowatisha itawafuata huko Misri na kugandamana nanyi, kwa hiyo ndiko, mtakakofia. Itakuwa hivyo: Watu wote waliozielekeza nyuso zao kwenda Misri, wakae ugenini huko, watauawa huko kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya; hawataona pa kuponea wala pa kuyakimbilia mabaya, mimi nitakayowaletea. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Kama makali yangu yenye moto yalivyomwagiwa wakaao Yerusalemu, ndivyo, mtakavyomwagiwa makali yangu nanyi, mtakapokwenda Misri. Nanyi mtaapizwa kwa kustukiwa, mtazomelewa na kutukanwa, lakini mahali hapa hamtapaona tena. Bwana anawaambia ninyi mlio masao ya Yuda: Msiende Misri! Yajueni kabisa, ya kuwa nimewashuhudia leo! Msiposikia mtazipoteza roho zenu, kwani ninyi wenyewe mmenituma kwa Bwana Mungu wenu kwamba: Tuombee sisi kwa Bwana Mungu wetu! Nayo yote, Bwana Mungu wetu atakayotuambia, tutayafanya vivyo hivyo, kama atakavyotujulisha. Nikawajulisha leo, lakini hamwisikii sauti ya Bwana Mungu wenu na kuyafanya yote, aliyonituma kuwaambia. Kwa hiyo jueni sasa: Panga na njaa na magonjwa mabaya ndiyo yatakayowaua mahali hapo panapowapendeza kupaendea na kukaa ugenini kuko huko. Ikawa, Yeremia alipokwisha kuwaambia watu wote wa ukoo huu maneno yote ya Bwana Mungu wao, ndiyo maneno yale yote, yeye Bwana Mungu wao aliyomtuma kuwaambia, ndipo, Azaria, mwana wa Hosaya, na Yohana, mwana wa Karea, na watu wote waliojivuna walipomwambia Yeremia: Wewe umesema uwongo, Bwana Mungu wetu hakukutuma kutuambia: Msiende Misri kukaa ugenini huko! Kwani Baruku, mwana wa Neria, anakushurutisha, utupingie, apate kututia mikononi mwa Wakasidi, watuue, wengine watuteke na kutupeleka Babeli. Basi, Yohana, mwana wa Karea, nao wakuu wote wa vikosi nao watu wote wa ukoo huu hawakuisikia sauti ya Bwana, wakae katika nchi ya Yuda. Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa vikosi wakayachukua masao yote ya Wayuda waliorudi kukaa katika nchi ya Yuda wakitoka kwa mataifa yote, walikotupiwa. Wakawachukua waume na wake na watoto na wana wa kike wa mfalme nao wote pia, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, aliowaacha na Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Safani, hata mfumbuaji Yeremia na Baruku, mwana wa Neria. Wakaja katika nchi ya Misri, kwani hawakuisikia sauti ya Bwana, wakakaa Tahapanesi. Neno la Bwana likamjia Yeremia huko Tahapanesi kwamba: Chukua kwa mkono wako mawe makubwa, uyafukie katika udongo penye tanuru lililoko pa kuiingilia nyumba ya Farao huku Tahapanesi, watu wa Yuda wakitazama! Kisha uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaniona, ninavyomtuma na kumchukua mtumishi wangu Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, nikiweka kiti chake cha kifalme juu ya mawe haya, niliyoyafukia, naye ataliwamba hema lake lenye utukufu juu yao. Atakuja kuipiga nchi hii ya Misri, nao walio wa kufa watakufa, nao walio wa kutekwa watatekwa, nao walio wa upanga watapigwa na upanga. Namo katika nyumba za miungu ya Misri nitatia moto, naye ataziteketeza, nayo miungu ataiteka; atajivika nchi ya Misri, kama mchungaj anavyojivika nguo yake, kisha atatoka huku na kutengemana. Lakini nguzo za nyumba ya kulitambikia jua iliyoko katika nchi ya Misri atazivunja, nazo nyumba za miungu ya Misri ataziteketeza kwa moto. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kuwaambia Wayuda wote waliokaa katika nchi ya Misri, ndio waliokaa Migidoli na Tahapanesi na Nofu na katika nchi ya Patirosi, la kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Ninyi mmeyaona hayo mabaya yote, niliyouletea Yerusalemu nayo miji yote ya Yuda, mkaiona, ya kuwa leo ni mavunjiko tu, hamna akaaye humo kwa ajili ya mabaya yao, waliyoyafanya ya kunikasirisha, walipokwenda kuvukizia na kutumikia miungu mingine, wasiyoijua wenyewe, wala ninyi wala baba zenu. Nami nilituma kwenu watumishi wangu wote waliokuwa wafumbuaji pasipo kuchoka kila kulipokucha kuwaambia: Msilifanye neno hilo la kutapisha, ninalochukizwa nalo! Lakini hawakusikia, wala hawakuyatega masikio yao, warudi na kuyaacha mabaya yao, wasivukizie miungu mingine. Ndipo, makali yangu yenye moto yalipomwagika, moto ukawaka katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu, hiyo miji ikawa mavunjiko na mahame, kama inavyojulikana leo. Sasa hivi ndivyo, Bwana Mungu Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mbona mnazifanyizia roho zenu mabaya makuu, mwang'oe kwenu waume na wake, vijana na wachanga, watoweke katikati ya Wayuda, kwenu lisisalie hata sao? Mbona mnanikasirisha kwa matendo ya mikono yenu, mkivukizia miungu mingine huku katika nchi ya Misri, mlikokuja kukaa ugenini tu? Mbona mnataka kujing'oa wenyewe, kusudi mwe wa kuapizwa na wa kutukanwa na mataifa yote ya huku nchini? Je? Mmeyasahau mabaya ya baba zenu na mabaya ya wafalme wa Yuda na mabaya ya wake zao na mabaya yenu na mabaya ya wake zenu, waliyoyafanya katika nchi ya Yuda namo barabarani mwa Yerusalemu? Mpaka siku hii ya leo hawajanyenyekea, wala hawakuogopa, kwani hawaendelei kwa Maonyo wala kwa maongozi yangu, niliyowapa ninyi na baba zenu, yawe machoni penu. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaniona, nikiwaelekezea uso wangu, niwafanyizie mabaya na kuwang'oa Wayuda wote pia. Nitawachukua masao ya Wayuda waliozielekeza nyuso zao kuja katika nchi ya Misri kukaa ugenini huku. Watamalizika wote katika nchi ya Misri, wakiuawa kwa panga na kwa njaa; kwa hiyo watamalizika wadogo kwa wakubwa wakifa kwa panga na kwa njaa; nao wataapizwa kwa kustukiwa, watazomelewa na kutukanwa, nikiwapatiliza wakaao katika nchi ya Misri, kama nilivyowapatiliza Wayerusalemu kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya. Hawatapata pa kuponea wala pa kukimbilia wale walio masao ya Wayuda waliokuja katika nchi ya Misri kukaa ugenini huku, wapate kurudi halafu katika nchi ya Yuda, roho zao zinayoitunukia, warudi huko na kukaa; kwani hawatarudi, isipokuwa watoro tu. Wakamjibu Yeremia waume wote waliojua, ya kuwa wake zao huvukizia miungu mingine, nao wake wote waliosimama hapo mkutano mkubwa, nao wote wa ukoo huu waliokaa Patirosi katika nchi ya Misri, wakasema: Neno hili, ulilotuambia katika Jina la Bwana, kwetu sisi hakuna atakayekusikia. Kwani tutayafanya kabisa maneno yote yaliyotoka vinywani mwetu, tumvukizie mfalme wa kike wa mbinguni na kummwagia vinywaji vya tambiko, kama tulivyofanya sisi na baba zetu na wafalme wetu na wakuu wetu katika miji ya Yuda namo barabarani mwa Yerusalemu, tukashiba vyakula, tukafanikiwa, lakini mabaya hatukuyaona. Toka hapo, tulipoacha kumvukizia mfalme wa kike wa mbinguni na kummwagia vinywaji vya tambiko, ndipo, tulipokosa yote, tukamalizika kwa panga na kwa njaa. Tena tukimvukizia mfalme wa kike wa mbinguni na kummwagia vinywaji vya tambiko, je? Waume wetu hawako, tukimtengenezea mikate yenye mifano yake na kummwagia vinywaji vya tambiko? Yeremia akawaambia watu wote wa ukoo huu, waume kwa wake na watu wote pia waliomjibu neno hilo, akasema: Kweli mmevukiza mavukizo katika miji ya Yuda namo barabarani mwa Yerusalemu ninyi na baba zenu, wafalme wenu na wakuu wenu nao watu wote waliokuwako katika nchi. Lakini hayo ndiyo, Bwana aliyoyakumbuka, akayaweka moyoni mwake. Kwa hiyo Bwana hakuweza kuvumilia tena kwa ajili ya ubaya wa matendo yenu na kwa ajili ya matapisho, mliyoyafanya; ndipo, nchi ilipogeuka kuwa mavunjiko na mapori tu, ikaapizwa, pasiwepo aikaaye, kama ilivyo siku hizi. Kwa kuwa mmevukiza na kumkosea Bwana, mkakataa kuisikia sauti yake na kuendelea kwa Maonyo yake na kwa maongozi yake na kwa mashuhuda yake, kwa sababu hii yamewafikia haya mabaya, mnayoyaona siku hizi. Yeremia akawaambia waume wote wa ukoo huu nao wake wote: Lisikieni neno la Bwana, ninyi Wayuda wote mlioko katika nchi ya Misri! Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema kwamba: Ninyi na wake zenu mliyoyasema kwa vinywa vyenu, myamalize kwa mikono yenu, yale ya kwamba: Tutayafanya kabisa maagano yetu, tuliyoyaapiana ya kumvukizia mfalme wa kike wa mbinguni na kummwagia vinywaji vya tambiko, basi, vitimizeni viapo vyenu! Vifanyizeni kabisa hivyo viapo vyenu! Lakini lisikieni neno la Bwana, ninyi Wayuda wote mkaao katika nchi ya Misri! Bwana anasema: Tazameni, nimeapa katika Jina langu kubwa kwamba: Jina langu lisitajwe tena katika nchi yote ya Misri vinywani mwa watu wa Kiyuda wo wote wakisema: Hivyo, Bwana Mungu alivyo Mwenye uzima! Mtaniona, nikiwa macho kuyaangalia mabaya, nitakayowafanyizia, siyo mema! Ndipo, watakapomalizika watu wote wa Kiyuda walioko katika nchi ya Misri kwa panga na kwa njaa, mpaka watakapokuwa wamekwisha. Nao watakaopona panga watatoka katika nchi ya Misri, warudi katika nchi ya Yuda, lakini watakuwa wachache sana, mkiwahesabu. Ndipo, masao yote ya Yuda waliokuja Misri kukaa ugenini huku watakapojua, kama ni neno lipi litakalosimama, langu au lao. Ndivyo, asemavyo Bwana: Hiki kitakuwa kielekezo chenu cha kwamba: Mimi nitawapatiliza mahali hapa, kusudi mjue, ya kuwa maneno yangu hutimilika kweli na kuwapatia mabaya. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikimtia Farao Hofura, mfalme wa Misri, mikononi mwa adui zake namo mikononi mwao wanaoitafuta roho yake, kama nilivyomtia Sedekia, mfalme wa Yuda, mkononi mwa adui yake Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, aliyeitafuta roho yake. Hili ndilo neno, mfumbuaji Yeremia alilomwambia Baruku, mwana wa Neria, alipoyaandika maneno haya katika kitabu, Yeremia akiyasema kwa kinywa chake, katika mwaka wa nne wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, akimwambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyokuambia Baruku: Unasema: Yamenipata, kwani Bwana anayaongeza maumivu yangu na kunitia majonzi! Nimechoka kwa kupiga kite, sioni pa kutulia. Utamwambia hivyo: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Unaniona mimi, ninavyoyabomoa, niliyoyajenga, ninavyoyang'oa, niliyoyapanda! Vinakuwa hivyo katika nchi yote nzima. Inakuwaje, wewe ukijitakia mambo makuu? Usijitakie hayo! Unaniona, ninavyowaletea mabaya wote wenye miili ya nyama, ndivyo, asemavyo Bwana; lakini wewe nitakupa roho yako kuwa pato lako mahali po pote, utakapokwenda. Hili ndilo neno la Bwana lililomjia mfumbuaji Yeremia kwa ajili ya wamizimu. Yatakayowapata Wamisri. Kwa ajili ya vikosi vya Farao Neko, mfalme wa Misri, vilivyokuwa Karkemisi penye mto wa Furati, vilipopigwa na Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, katika mwaka wa nne wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, anasema: Tengenezeni ngao ndogo na kubwa, mwende vitani! Watandikeni farasi, wapandeni, ninyi wapanda farasi! Jipangeni, wenye kofia za chuma vichwani! Inoeni mikuki, kisha zivaeni shati za chuma! Mbona ninawaona hawa, wakirudi nyuma kwa kustuka? Mbona wanguvu wao wamepondeka, wakakimbia sana pasipo kugeuka? Matisho po pote! ndivyo, asemavyo Bwana. Lakini naye mwenye miguu miepesi hatakimbia, wala mwenye nguvu hatapona. Upande wa kaskazini kando ya mto wa Furati wamejikwaa, wakaanguka. Alikuwa nani aliyepanda kama mto wa Nili, maji yake yakajirusha kama ya mito mikubwa? Mmisri alipanda kama mto wa Nili, maji yakajirusha kama ya mito mikubwa, akasema: Nitapanda kuifunikiza nchi, niangamize mji nao wakaao humo! Pandeni, ninyi farasi! Pigeni mbio kama wenye wazimu, ninyi magari! Wapiga vita na watokee, wale Wanubi na Waputi washikao ngao na Waludi washikao pindi, wajuao kuzivuta! Siku hii ni yake Bwana Mungu Mwenye vikosi, ni siku ya lipizi ya kuwalipiza wapingani wake, panga zitakula, zishibe, mpaka zilewe kwa damu zao, kwani wao ndio kama ng'ombe za kumtambikia Bwana Mungu Mwenye vikosi katika nchi ya upande wa kaskazini kwenye mto wa Furati. Pandeni Gileadi kuchukua mafuta ya kwaju, ninyi wanawali mliozaliwa Misri! Ni bure, ukitumia dawa nyingi, hakuna itakayokuponya. Mataifa yameyasikia yakutiayo soni, vilio vyako vimeijaza nchi. Kwani mpiga vita amejikwaa kwa mpiga vita mwenziwe, wakaanguka wote wawili pamoja. Hili ndilo neno, Bwana alilomwambia mfumbuaji Yeremia, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alipokuja kuipiga nchi ya Misri: Pigeni mbiu huko Misri na kuitangaza Migidoli! Tena itangazeni Nofu na Tahapanesi kwamba: Jipangeni na kujitengeneza! Kwani panga zimewala waliokuzunguka. Mbona watukufu wako wamelazwa chini? Hawakusimama, kwani Bwana aliwakumba; akakwaza wengi, wakaangukiana mtu na mwenziwe wakiambiana: Inuka, turudi kwetu kwa wenzetu wa ukoo katika nchi, tulikozaliwa, tuzikimbie panga za wanguvu! Ndiko, walikomwita Farao, mfalme wa Misri: Angamio, ameikosa siku yake ya kupona! Ndivyo, asemavyo Mfalme, Jina lake Bwana Mwenye vikosi: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, atakuja afananaye na Tabori ulio mkuu wa kuipita milima mingine au na Karmeli huko pwani. Jifanyizieni vyombo vya kwenda navyo mkitekwa, ninyi wanawali mkaao Misri! Kwani Nofu utakuwa mahame tu kwa kuteketea, msikae mtu. Misri ni mori mzuri mno, lakini mbung'o anakuja upesi toka kaskazini. Nao warugaruga wao waliokuwa kwao kama ndama wenye manono, hao nao wamegeuka, wakakimbia wote pamoja, hawakusimama, kwani siku ya kuangamia kwao iliwafikia, ndio wakati wa kupatilizwa kwao. Mashindo yao yakawa kama ya nyoka akikimbia, kwani wale wanakuja na vikosi vyao, wanawajia wakishika mashoka kama wakata kuni. Ndivyo, asemavyo Bwana: Wataikata misitu yao isiyochunguzika, kwani ni wengi kuliko nzige, hawahesabiki. Wanawali wa Misri, wamepatwa na soni kwa kutiwa mikononi mwa watu waliotoka kaskazini. Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anasema: Mtaniona, ninavyompatiliza Amoni wa No naye Farao na nchi yake ya Misri hata miungu yake na wafalme wake; nitampatiliza Farao kweli nao wote wamwegemeao. Nitawatia mikononi mwao wanaozitafuta roho zao, namo mikononi mwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, namo mikononi mwa watumishi wake. Lakini hayo yatakapokwisha, nchi itakaa watu kama siku za kale; ndivyo, asemavyo Bwana. Wewe mtumishi wangu Yakobo, usiogope! Nawe Isiraeli, usistuke! Kwani utaniona, nikikuokoa na kukutoa huko mbali, nao walio kizazi chako nitawatoa katika ile nchi, walikopelekwa kwa kutekwa. Yakobo atarudi, akae na kutulia pasipo kuhangaika, kwani hakuna atakayemstusha. Ndivyo, asemavyo Bwana: Wewe ntumishi wangu Yakobo, usiogope! Kwani mimi niko pamoja na wewe, kwani nitayamaliza mataifa yote, ambayo nimekutupa kwao, lakini wewe sitakumaliza, nitakuchapa tu, kama yakupasavyo, nisikuache pasipo patilizo lo lote. Hili ndilo neno la Bwana lililomjia mfumbuaji Yeremia kwa ajili ya Wafilisti, Farao alipokuwa hajaupiga Gaza. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaona, maji yatakapokuja na kutoka kaskazini, yatakuwa mto ufurikao, yataifunikiza nchi nayo yote yaliyomo, miji nao wakaamo. Ndipo, watu watakapopiga makelele, watalia wote wakaao katika nchi hiyo. Kwa mashindo ya farasi wao wenye nguvu, wakipiga kwato zao, na kwa makelele ya magari yao na kwa uvumi wa magurudumu yao, baba hawatawageukia wana wao, kwani mikono itakuwa imewalegea. Kwani inakuja ile siku ya kuwaangamiza Wafilisti wote, ndiyo ya kuwang'olea Watiro na Wasidoni wasaidiaji wote waliosalia; ndipo, Bwana atakapowaangamiza Wafilisti walio masao yao waliokitoka kisiwa cha Kafutori. Wagaza watajinyoa vichwa, Waaskaloni pamoja nao waliosalia bondeni kwao watanyamazishwa, watajikata chale, mpaka lini? Mpaka lini upanga wake Bwana utakuwa hautulii? Jirudie alani mwako, upumzike na kunyamaza! Lakini utawezaje kutulia, Bwana akiuagiza kufanya kazi yake? Askaloni na pwani ndiko, Bwana alikoutuma. Yatakayowapata Wamoabu. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Nebo yameupata, kwani umebomolewa! Kiriatemu umepatwa na soni kwa kutekwa, kweli boma lake lililokuwa mlimani limepatwa na soni kwa kustuka. Hakuna tena utukufu wa Moabu; mle Hesiboni wanawawazia mabaya kwamba: Twende, tuwang'oe, wasiwe kabila! Nawe Madimeni, utanyamazishwa, panga zitakufuata nyuma. Toka Horonemu kunasikilika makelele, maangamizo na mavunjiko ni makubwa. Wamoabu wamevunjika, vilio vinasikilika hata Soari. Kwani njia ya kupandia Luhiti wanaipanda na kulia, hata katika njia ya kutelemkia toka Horonemu kunasikilika yowe zao wasongekao kwa ajili ya mavunjiko kwamba: Kimbieni! Ziponyeni roho zenu! Mwe kama mti wa nyikani usio na majani! Kwa kuwa unayaegemea matendo yako na vilimbiko vyako, wewe nawe utatekwa, naye Kemosi hana budi kwenda kuhamishwa pamoja na watambikaji wake na wakuu wake. Mwangamizaji ataujia kila mji, hakuna mji utakaopona, penye bonde pataangamia, napo penye mbuga pataharibika, kama Bwana alivyosema. Wapeni Wamoabu mabawa, watoke na kuruka! Kwani miji yao itakuwa mapori, msikae mtu. Ameapizwa afanyaye kazi ya Bwana na kulegea! Ameapizwa auzuiaye upanga, usiue! Wamoabu walikaa pasipo kuhangaishwa tangu ujana wao, wakatulia penye mvinyo zao zenye shimbi, hawazitoi chomboni na kumimina katika kingine, wala hawajakwenda kuhamishwa; kwa hiyo yapendezayo vinywa vyao kuyala ni yaleyale, nayo yapendezayo pua zao kuyanusa hayakugeuka. Ndivyo, asemavyo Bwana: Kwa hiyo wataona, siku zikija, nitakapotuma kwao mafundi wa mvinyo, watavipindua vyombo vyao na kuzimwaga mvinyo zilizomo, kisha wataivunja hiyo mitungi yao. Ndipo, Wamoabu watakapoona soni kwa ajili ya Kemosi, kama walio wa mlango wa Isiraeli walivyoona soni kwa ajili ya Beteli mlimokuwa na egemeo lao. Mwasemaje: Sisi tu wenye nguvu, tu mafundi wa kupiga vita? Wamoabu wataangamia, miji yao itapandiwa, nao vijana wao waliochaguliwa watakuwa hawana budi kutelemka, wauawe; ndivyo, asemavyo Mfalme, Jina lake ni Bwana Mwenye vikosi. Angamio lao Wamoabu liko karibu, mabaya yao yanakuja upesi sana. Nyote mkaao na kuwazunguka waombolezeeni pamoja nao wote walijuao jina lao! Semeni: Kumbe fimbo yenye nguvu imevunjika! Nayo ilikuwa bakora yenye utukufu! Ondokeni penye utukufu, mkae mchangani penye ugumu, ninyi wanawali mkaao Diboni! Kwani mwenye kuwaangamiza Wamoabu anapanda kufika kwako, ayabomoe maboma yako! Ninyi mkaao Aroeri, simameni njiani na kupeleleza mkiwauliza watoro walioepuka, mkisema: Kumetendeka nini? Wamoabu wamepatwa na soni kwa kuvunjika; lieni na kupaza sauti: Yatangazeni kwenye Arnoni, ya kuwa Wamoabu wameangamia! Mapatilizo yameijia nchi yenye mbuga huko Holoni na Yasa na Mefati, na Diboni na Nebo na Beti-Dibulatemu, na Kiriatemu na Beti-Gamuli na Beti-Meoni, na Kirioti na Bosira na miji yote ya nchi ya Moabu iliyoko mbali, nayo iliyoko karibu. Pembe ya Moabu imekatwa, nao mkono wake umevunjwa; ndivyo, asemavyo Bwana. Walevyeni! Kwani wamejikuza kuliko Bwana; na waanguke kifudifudi katika matapiko yao, wachekwe nao hao! Au Waisiraeli hawakuchekwa kwenu? Je? Walionwa kwenye wezi, mkiwatingishia vichwa kila mlipowataja? Ninyi mkaao Moabu, tokeni mijini, mkae magengeni, mwe kama hua wanaojenga matundu yao juu penye miamba iliyokatika. Tumesikia, ya kuwa Wamoabu walijivuna sanasana, wakajikuza kwa kujivuna kwao, kwa kiburi chao wakawaza makuu mioyoni mwao. Ndivyo, asemavyo Bwana: Mimi nimeyajua makorofi yao, ya kuwa hayana maana, nayo maneno yao makuu, ya kuwa hawakuyafanya. Kwa hiyo ninawalilia Wamoabu, ninawapigia Wamoabu wote makelele; wengine wanawapigia kite watu wa Kiri-Heresi. Kuliko Yazeri ninawalilia ninyi mizabibu ya Sibuma, matawi yenu yaliendelea kufika baharini, yalifika kweli kwenye bahari ya Yazeri; siku za kiangazi walipochuma zabibu zenu, mara mwangamizaji akaja. Ndipo, shangwe za furaha zilipotoweka Karmeli na katika nchi ya Moabu. Nayo mvinyo iliyokuwa kamulioni nikaikomesha, hawakamui tena kwa kupiga shangwe; shangwe zao sizo shangwe tena. Toka Hesiboni wanapiga makelele, hata Elale na Yasa wanapaza sauti zao, tena toka Soari hata Horonemu na Eglati-Selisia hulia, ya kuwa nayo maji ya Nimurimu yatakuwa yamekauka. Ndivyo, asemavyo Bwana: Nitawakomesha Wamoabu, wasipande vilimani kuivukizia miungu yao. Kwa hiyo moyo wangu unawapigia Wamoabu kite na kuvuma kama zomari, nao watu wa Kiri-Heresi moyo wangu unawapigia kite na kuvuma kama zomari, kwa kuwa mapato waliyojipatia yamepotea. Kwani vichwa vyote vitakuwa vyenye vipara, nazo ndevu zote zitakuwa zimenyolewa, nayo mikono yote itakuwa yenye chale, navyo viuno vyote vitakuwa na magunia. Po pote vipaani katika nchi ya Moabu napo barabarani po pote patakuwa na maombolezo, kwani nitawavunja Wamoabu, kama ni chombo kisichopendeza; ndivyo, asemavyo Bwana. Kumbe wamevunjika! Pigeni vilio! Kumbe Wamoabu wamezigeuza kosi zao kwa soni! Tangu hapo Wamoabu watakuwa kicheko na kitisho kwao wote wakaao na kuwazunguka. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazameni, anawarukia Wamoabu kama kozi na kuwakunjulia mabawa yake. Kirioti umetekwa, nayo miji yenye maboma imechukuliwa; kwa hiyo mioyo ya wapiga vita wa Moabu itakuwa siku ile kama moyo wa mwanamke anayetaka kuzaa. Wamoabu wataangamizwa, wasiwe taifa tena, kwa kuwa wamejikuza kuliko Mungu. Mastuko na miina na matanzi yatawapata ninyi mkaao Moabu; ndivyo, asemavyo Bwana. Ayakimbiaye mastuko ataanguka mwinani; atokaye mwinani atakamatwa na tanzi; haya yatakuwa hapo, nitakapowatimilizia hao Wamoabu mwaka wa mapatilizo yao; ndivyo, asemavyo Bwana. Watoro wakisimama kivulini kwenye Hesiboni kwa kuishiwa nguvu, moto utatoka Hesiboni namo Sihoni kati, moto uwakao sana utatoka, utavila vipanja vya Wamoabu nazo tosi zao wapigao vita. Yatawapata, ninyi Wamoabu! Ukoo wake Kemosi utaangamia! Kwani wanao wa kiume watachukuliwa kwenda utumwani, nao wanao wa kike watakwenda kuwa vijakazi. Kisha nitayafungua mafungo ya Moabu, siku zitakapotimia; ndivyo, asemavyo Bwana. Mpaka hapa ni hukumu za Moabu. Yatakayowapata wana wa Amoni. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Je? Hakuna wana kwao Waisiraeli? Hakuna awezaye kulichukua fungu lake? Mbona Malkamu ameichukua nchi ya Gadi nao watu wa ukoo wake wanakaa katika miji yao? Ndivyo, asemavyo Bwana: Wataona, siku zikija, nitakapovumisha makelele ya vita huko Rabati ulio mji wa wana wa Amoni, nao utakuwa machungu ya mabomoko, nayo miji ya wana wao itateketezwa kwa moto; ndipo, Waisiraeli watakapoyachukua mafungu yao kwao walioyachukua. Ndivyo, Bwana anavyosema: Pigeni vilio, ninyi wa Hesiboni, ya kuwa Ai umebomolewa! Pigeni makelele, ninyi wanawali wa Raba! Jifungeni magunia! Ombolezeni na kwenda huko na huko penye nyua! Kwani Malkamu atakwenda kutekwa na kuhamishwa pamoja na watambikaji wake na wakuu wake. Mnayasifiaje mabonde zaidi, mlio na bonde lichuruzikalo maji, ninyi wanawali wakatavu? Mnaviegemea vilimbiko vyenu kwamba: Yuko nani atakayenijia? Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Mwenye vikosi: Mtaniona, nikiwaletea mastusho toka pande zote pia, nanyi mtafukuzwa, kila mtu akimbie pasipo kutazama nyuma, tena hatakuwako atakayewakusanya hao watoro. Hayo yatakapokwisha, nitayafungua mafungo ya wana wa Amoni. Yatakayowapata Waedomu. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Je? Huko Temani hakuna tena werevu wa kweli? Wajuzi wamepotelewa na akili, werevu wao wa kweli ukatoweka? Kimbieni, mtoroke! Chimbeni mashimo ya kukaa ndani yao, ninyi mkaao Dedani! Kwani nitawaletea angamio la Esau siku ya kuwapatiliza. Kama wachuma zabibu wanakujia, hawasazi za kuokoteza; kama wezi wanakujia na usiku, hupokonya, mpaka wakitoshewa. Kwani mimi nimemvumbua Esau, nikayafunua maficho yake, asiweze kujificha tena. Kizazi chake kumeharibiwa pamoja na ndugu zake, nao waliokaa nao hawako kabisa. Waacheni watoto wenu waliofiwa na wazazi! Mimi nitawatunza; nao wajane wenu na waniegemee! Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazama, wasiopaswa kukinywa kinywaji changu hawakuwa na budi kukinywa, nawe wewe usilipishwe? Nawe utalipishwa, kwani utakinywa! Ndivyo, asemavyo Bwana: Nimejiapia mwenyewe kwamba: Bosira sharti ustukiwe kwa kutiwa soni, ukae peke yake kwa kuapizwa, nayo miji yake yote itakuwa mabomoko kale na kale. Nimesikia mbiu kwake Bwana, mjumbe ametumwa kwenda kwa mataifa kwamba: Jikusanyeni, mwujie! Ondokeni kwenda vitani! Kwani mtaniona, nikiwafanya kuwa wadogo katika mataifa, mbezwe na watu! Kuogopesha kwenu ni majivuno tu ya mioyo yenu yaliyowadanganya, kwa kuwa mnakaa nyufani kwenye miamba, mkagandamana na milima mirefu. Lakini ijapo mvijenge vituo vyenu juu kabisa kama tai, huko nako nitawashusha; ndivyo, asemavyo Bwana. Nchi ya Edomu itakuwa mapori matupu, kila atakayepapita atastuka na kuyazomea mapigo yake yote. Bwana anasema: Kama Sodomu na Gomora ilivyoangamizwa pamoja na vijiji vyao, hivyo napo hapo hapatakaa mtu, wala hapatalala mgeni wa kimtu. Kama simba anavyopanda akitoka machakani kwenye Yordani, ajie maboma yenye nguvu, ndivyo, nitakavyowakimbiza kwao kwa mara moja, naye aliyechaguliwa nitamweka kuwa mkuu wao, kwani yuko nani afananaye na mimi? Au yuko nani atakayeniwekea siku? Yuko mchungaji gani atakayesimama usoni pangu? Kwa hiyo lisikieni shauri la Bwana, alilowakatia Waedomu, nayo mawazo yake, aliyowawazia wakaao Temani: kweli watakaowakokotakokota ndio wadogo wa makundi, kweli nchi yao yenyewe itawastukia. Kwa mtutumo wa kuanguka kwao nchi itatetemeka, nazo sauti za vilio vyao zitasikilika hata kwenye Bahari Nyekundu. Tazameni, anaurukia Bosira kama kozi na kuukunjulia mabawa yake. Kwa hiyo mioyo ya wapiga vita wa Edomu itakuwa siku ile kama moyo wa mwanamke anayetaka kuzaa. Yatakayoupata Damasko. Hamati na Arpadi wamepatwa na soni, kwani wamesikia mbiu mbaya, wakayeyuka na kuhangaika kama bahari isiyoweza kutulia. Wadamasko wamelegea, wakageuka, wakimbie, mtetemeko ukawashika, masongano na machungu yakawapata kama mwanamke anayetaka kuzaa. Kumbe umeachwa wote mji huo uliokuwa mji, walimoshangilia kwa kufurahi! Kwa hiyo wavulana wake wataanguka barabarani mwake, nao wapiga vita wote watanyamazishwa siku ile; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Kisha nitawakisha moto bomani mwa Damasko, uyale majumba ya Beni-hadadi. Yatakayoipata nchi ya Kedari nazo nchi za kifalme za Hasori, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alizozipiga. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Inukeni, mpande kwenda Kedari, mwaangamize wana wa nchi iliyoko maawioni kwa jua! Na wayachukue mahema yao na makundi yao, wajitwalie mazulia yao na vyombo vyao vyote na ngamia wao, nao watawalilia kwamba: Matisho po pote! Kimbieni na kupiga mbio sana! Chimbeni mashimo ya kukaa ndani yao, ninyi mkaao Hasori! ndivyo, asemavyo Bwana; kwani Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, amewakatia shauri na kuwawazia mawazo. Ndivyo, asemavyo Bwana: Inukeni, mpande kwenda kwa taifa lililojituliza na kukaa pasipo mahangaiko! Hawama milango wala makomeo, hujikalia peke yao tu. Ngamia wao watakuwa mateka yenu, nao kondoo na mbuzi wao wengi mno watakuwa mapato yenu. Wao wenyewe wanyoao denge nitawatawanya kwenda pande zote, upepo utokako, nikiwaletea maangamizo, yawatokee po pote; ndivyo, asemavyo Bwana. Ndipo, Hasori utakapokuwa kao la mbwa wa mwitu kwa kukaa peke yao tu kale na kale. Hapatakaa mtu, wala hapatalala mgeni wa kimtu. Hili ndilo neno la Bwana lililomjia mfumbuaji Yeremia kuwaambia Waelamu, Sedekia, mfalme wa Yuda, alipoanzia kuwa mfalme. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mtaniona, nikizivunja pindi zao Waelamu, nguvu zao nyingi zilimo. Nitawaletea Waelamu pepo nne zitokazo pande nne za mbinguni, niwatawanye kwenye hizo pepo, pasiwe taifa lisilojiwa na watoro wa nchi ya Elamu. Nitawastusha Waelamu, wawaogope adui zao nao wazitafutao roho zao; kisha nitawaletea mabaya, makali yangu yenye moto yatakapowawakia, mpaka niwamalize. Ndipo, nitakapokiweka kiti changu cha kifalme huko Elamu, nimwangamize mfalme na wakuu, watoweke huko; ndivyo, asemavyo Bwana. Lakini siku zitakapotimia, nitayafungua mafungo ya Waelamu; ndivyo, asemavyo Bwana. Hili ndilo neno, Bwana alilolisema kwa kinywa chake Yeremia kuwaambia Wababeli walioko katika nchi ya Wakasidi. Yatangazeni kwa mataifa, wayasikie! Twekeni bendera! Yasimulieni, msiyafiche! Semeni: Babeli umetekwa, Beli amepatwa na soni, Merodaki amestuka, vinyago vyao vimeumbuliwa, mifano yao imevunjika! Kwani taifa lililotoka upande wa kaskazini limewapandia, hilo limeiharibu nchi yao iwe peke yake, isikae tena wala mtu wala nyama, wamekimbia kwenda zao. Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku zile za wakati huo ndipo, wana wa Isiraeli pamoja na wana wa Yuda watakapokuja wakienda na kulia machozi; hivyo watakwenda kumtafuta Bwana Mungu wao. Watauliza njia ya kwenda Sioni; ndiko, nyuso zao zinakoelekea kwamba: Njoni kuandamana na Bwana, tukifanya agano la kale na kale lisilosahauliwa tena! Walio ukoo wangu walikuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao waliwapoteza, wakatangatanga milimani, walipotoka mlimani wakaendea kilima kingine, wakakisahau kituo chao. Wote waliowaona wakawala, nao waliowasonga wakasema: Hatukosi. Hayo yakawapata, kwa kuwa walimkosea Bwana aliyekuwa lisho lao la kweli, ni yeye Bwana, baba zao waliyomngojea. Kimbieni, mwutoke mji wa Babeli, mliomo! Itokeni nayo nchi ya Wakasidi, mwe kama madume ya kondoo wanaoyatangulia makundi! Kwani mtaniona mimi, nikiinua mkutano wa mataifa makubwa yatokayo upande wa kaskazinni, niyapandishe kwenda Babeli; watakapojipanga, hapohapo ndipo, utakapotekwa. Mishale yao ni kama ya mpiga vita mwerevu asiyerudi mikono mitupu. Nchi ya Wakasidi itatekwa, nao watakaoiteka watashiba wote; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwa kuwa mwalifurahi, mkapiga vigelegele hapo, mlipolipokonya fungu langu, mkachezacheza kama ndama wakipura, mkalia kama farasi wenye nguvu: mama yenu atapatwa na soni kabisa, yeye aliyewazaa ataiva uso; hapo mtaona, hilo taifa lililokuwa la mwisho linavyogeuka kuwa nyika kavu na jangwa. Kwa kukasirika kwake Bwana hautakaa mtu, wote pia utakuwa peke yake tu, kila atakayepapita palipokuwa na Babeli, atapastuka na kuuzomea kwa ajili ya mapigo yake yote. Jipangeni na kuuzunguka Babeli, ninyi nyote mpindao pindi! Upigeni mishale, msiitendee choyo! Kwani wamemkosea Mungu. Pigeni vigelegele po pote! Umejitia mikononi mwenu! Maboma yake yamebomolewa, kuta zake zimeangushwa, kwani hili ndilo lipizi la Bwana, kwa hiyo ulipisheni! Kama ulivyofanya, ufanyizieni! Huko Babeli wang'oeni wapanzi nao wavunaji washikao miundu siku za mavuno! Kwa kuzikimbia panga za wenye nguvu kila mtu atawageukia walio wa ukoo wake, kwa hiyo kila mtu ataikimbilia nchi ya kwao. Waisiraeli ni kama kondoo waliotawanyika kwa kufukuzwa na simba: kwanza mfalme wa Asuri aliwala, mwisho Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, aliwavunja mifupa. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaniona, nikimpatiliza mfalme wa Babeli na nchi yake, kama nilivyompatiliza mfalme wa Asuri. Nitawarudisha Waisiraeli kwao, walikokaa, wajilishe mazao ya Karmeli na ya Basani, roho zao zishibe milimani kwa Efuraimu nako huko Gileadi. Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku zile zitakapotimia, manza, Waisiraeli walizozikora, zitatafutwa, lakini zitakuwa haziko, nayo makosa ya Wayuda, lakini hayataonekana, kwani nitayaondoa kwao, nitakaowasaza. Ipandie nchi yenye makatavu mawili, uingie namo, wakaamo wenye kupatilizwa! Waue na kuwamaliza walio nyuma yao! Yafanye yote, kama nitakavyokuagiza! Sauti za vita zinasikilika katika nchi hii, nayo mavunjiko ni makubwa. Kumbe nyundo iliyozipiga nchi zote imepondeka kwa kuvunjikavunjika! Kumbe Babeli umegeuka kuwa wa kustukiwa na mataifa yote! Nimekutegea, wewe Babeli, ukanaswa, nawe ulikuwa huvijui; umeonwa, ukakamatwa, kwani umemtaka Bwana, mpigane. Bwana amelifungua limbiko lake, akayatoa mata ya makali yake, kwani yeye Bwana Mungu Mwenye vikosi yuko na kazi katika nchi ya Wakasidi. Njoni huku na kutoka kwenye mapeo ya nchi! Vifungueni vyanja vyake vya ngano, mzikusanye kuwa chungu, kisha zimalizeni kwa kuziteketeza, masao yasipatikane kamwe! Wachomeni ng'ombe wao wote kwa mikuki, waanguke kwa kuchinjwa hivyo, Watapatwa na mambo, kwani siku yao inakuja, watakapopatilizwa. Sauti zao walioitoka nchi ya Babeli kwa kukimbia mbio sana zinasikilika Sioni, wakiyatangaza malipizi ya Bwana Mungu wetu, jinsi alivyolilipizia Jumba lake takatifu! Waiteni wapiga mishale wote wanaopinda pindi, waje Babeli, wapige kambi zao kuuzunguka, usipate pa kukimbilia. Ulipisheni matendo yake! Yote, uliyoyafanya, ufanyizieni yaleyale! Kwani umejivuna kuwa mkuu kuliko Bwana, kuliko yeye aliye Mtakatifu wa Isiraeli. Kwa hiyo vijana wako wataangushwa barabarani mwako, nao waume wote wa kupiga vita watanyamazishwa siku hiyo; ndivyo, asemavyo Bwana. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Mwenye vikosi: Utaniona, nikikujia, wewe mkorofi; kwani itakuja siku yako, nitakapokupatiliza. Ndipo, mkorofi atakapojikwaa, aanguke, lakini hatakuwako atakayemwinua; mijini mwake nitawasha moto, uiteketeze yote pande zake zote. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Wameteseka wana wa Isiraeli pamoja na wana wa Yuda; wote waliowateka na kuwahamisha wanawashika, wakakataa kuwapa ruhusa kwenda. Lakini mkombozi wao ni mwenye nguvu, Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake. Yeye atawagombea hayo magomvi yao, kusudi aitulize nchi, lakini wakaao Babeli atawahangaisha. Ndivyo, asemavyo Bwana: Panga na ziwajie Wakasidi nao wakaao Babeli nao wakuu wao nao werevu wao wa kweli! Panga na ziwajie wapuzi, wapumbae! Panga na ziwajie wapiga vita wao, wazimie kwa kustuka! Panga na ziwajie farasi wao na magari yao nao warugaruga walio katikati yao, wawe kama wanawake! Panga na zivijie navyo vilimbiko vyao, vipokonywe! Jua kali na liyapige maji yao, yakauke! Kwani nchi hii ni ya vinyago, nao wenyeji wameingiwa na wazimu kwa ajili ya mifano yao. Kwa hiyo watakaa humo nyama wa porini na mbwa wa mwitu, nao mbuni watakaa mwake, lakini watu hawatakaa humo kale na kale, ila utakaa pasipo mtu kwa vizazi na vizazi. Ndivyo, asemavyo Bwana: Kama Mungu alivyoangamiza Sodomu na Gomora pamoja na vijiji vyao, hivyo napo hapa hapatakaa mtu, wala hapatalala mgeni wa kimtu. Utaona, watu wakija toka kaskazini, tena taifa kubwa na wafalme wengi watainuka mapeoni kwa nchi. Wanashika pindi na mikuki, ni wakorofi, hawana huruma, sauti zao huvuma kama bahari, hupanda farasi, wako tayari kupiga kama mtu wa vitani; wanakujia wewe, binti Babeli. Mfalme wa Babeli amezisikia habari zao; ndipo, mikono yake ilipolegea, masongano yakamshika na uchungu, kama mwanamke anayetaka kuzaa. Kama simba anavyopanda akitoka machakani kwenye Yordani, ajie maboma yenye nguvu, ndivyo, nitakavyowakimbiza kwao kwa mara moja, naye aliyechaguliwa nitamweka kuwa mkuu wao, kwani yuko nani afananaye na mimi? Au yuko nani atakayeniwekea siku? Yuko mchungaji gani atakayesimama usoni pangu? Kwa hiyo lisikieni shauri la Bwana, aliloukatia Babeli, nayo mawazo yake, aliyoiwazia nchi ya Wakasidi kwamba: kweli watakaowakokotakokota ndio wadogo wa makundi, kweli nchi yao yenyewe itawastukia. Kwa mtutumo wa kutekwa kwa Babeli nchi itatetemeka, navyo vilio vitasikilika kwa mataifa. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikiinua upepo uangamizao, uujie Babeli nao wakaamo walio wenye mioyo ya kuniinukia. Nitatuma wenye nyungo kwenda Babeli, waupepete, kisha watazichukua mali za nchi, kwani siku ile mbaya watazunguka mjini po pote. Hapo hatakuwako mwenye upindi atakayewapiga mshale, wala hatakuwako mwenye shati ya chuma atakayeweza kuwainukia. Lakini msiwaonee uchungu vijana wake! Ila wao wote wa vikosi vyao watieni mwiko wa kuwapo! Hivyo wataanguka tu katika nchi ya Wakasidi waliopata vidonda, nao waliochomwa watalala huko barabarani. Kwani Isiraeli na Yuda hawakuachwa na Mungu wao aliye Bwana Mwenye vikosi, wawe wajane, ila nchi yao wale ilijaa maovu, waliyomkosea Mtakatifu wa Isiraeli. Kimbieni na kutoka mwake Babeli, kila mtu aiponye roho yake, msinyamazishwe kwa ajili ya manza, walizozikora wao! Kwani hii ndiyo siku ya lipizi ya Bwana, awalipishe matendo yao. Babeli ulikuwa kinyweo cha dhahabu mkononi mwa Bwana kilichozilevya nchi zote; mvinyo yake mataifa yaliinywa, kwa hiyo mataifa yakaingiwa na wazimu. Mara Babeli umeanguka, ukavunjika! Ulilieni! Leteni mafuta ya kwaju kuyatia penye madonda yake! Labda utapona. Tulitaka kuuponya Babeli, lakini haukuponyeka; basi, uacheni, twende kila mtu katika nchi ya kwao! Kwani hukumu yake inafika hata mbinguni, inakwenda juu mpaka kwenye mawingu. Bwana ameyatokeza, ya kuwa mambo yetu yameongoka; njoni, tusimulie Sioni, Bwana Mungu wetu aliyoyafanya. Inoeni mishale! Zishikeni ngao! Bwana ameziinua roho za wafalme wa Wamedi, kwani mawazo yake yameuelekea Babeli, auangamize, kwani hili ndilo lipizi lake Bwana, alilipizie Jumba lake takatifu. Twekeni bendera zielekeazo kuta za Babeli! Malindo yatieni nguvu mkiongeza walinzi na kuweka nao wenye kuvizia! Kwani Bwana aliyoyawaza huyafanya, ayatimize nayo yale, aliyoyasema, ya kuwa atawafanyizia wakaao Babeli. Unakaa penye maji mengi, unavyo vilimbiko, lakini mwisho wako umefika, ndipo hapo palipopimiwa choyo chako. Bwana Mwenye vikosi amejiapia mwenyewe kwamba: Ijapo nimekujaza watu kama nzige, itakuwa, wakuzomee kwa kukushinda. Yeye ndiye aliyeifanya nchi kwa uwezo wake, akausimika ulimwengu kwa werevu wake wa kweli, akazitanda mbingu kwa utambuzi wake. Huvumisha maji mbinguni kwa ngurumo na kupandisha mawingu yatokayo mapeoni kwa nchi, kisha hupiga umeme kwenye mvua na kutoa upepo huko, alikouweka. Ndipo, kila mtu anapopumbaa tu, asijue yatokako, hata kila mfua dhahabu hupatwa na soni kwa ajili ya kinyago chake, kwani alichokitengeneza ni uwongo tu, hata pumzi haimo. Havina maana, ni kazi ya kuchekwa tu; siku vitakapopatilizwa huangamia. Lakini aliye fungu lake Yakobo hafanani navyo, kwani yeye ndiye aliyeyatengeneza yote, naye Isiraeli ni ukoo uliopata fungu kwake; Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake. Kweli ulikuwa nyundo yangu, nikakutumia kuwa chombo cha vita; hivyo nikaponda mataifa, nikaangamiza nchi za kifalme kwa kukutumia. Nikaponda farasi pamoja nao waliowapanda kwa kukutumia, nikaponda magari nao walioyapanda kwa kukutumia. Nikaponda waume na wake kwa kukutumia, nikaponda wazee na wana kwa kukutumia, nikaponda wavulana na wasichana kwa kukutumia. Nikaponda wachungaji na makundi yao kwa kukutumia, nikaponda wakulima pamoja na ng'ombe wao wa kulima kwa kukutumia, nikaponda watawala nchi na wakuu kwa kukutumia. Lakini machoni penu nitaulipisha Babeli pamoja nao wote wakaao katika nchi ya Wakasidi mabaya yao yote, waliyoyafanya huko Sioni; ndivyo, asemavyo Bwana. Ndivyo, asemavyo Bwana: Utaniona, nikikujia wewe, mlima uangamizao! Umeziangamiza nchi zote, lakini nimekukunjulia mkono wangu, nikuporomoshe, utoke miambani; nitakugeuza kuwa mlima uliochomwa moto. Hawatachukua kwako mawe ya pembeni wala ya msingi, kwani utakuwa jangwa la kale na kale; ndivyo, asemavyo Bwana. Twekeni bendera katika nchi hii! Pigeni mabaragumu kwa mataifa! Yaeueni mataifa, yaujie! Ziiteni nchi za kifalme za Ararati na za Mini na za Askenazi, ziujie! Wekeni mkuu wa vita, aupige! Pandisheni farasi walio wengi kama nzige wenye manyoya! Yaeueni mataifa, yaujie, wafalme wa Wamedi nao watawala nchi wa kwao nao wakuu wao wote na nchi zote za ufalme wao! Ndipo, nchi itakapotetemeka kwa kustuka, kwani mawazo yake Bwana yameuinukia Babeli kuigeuza nchi ya Babeli kuwa peke yake tu, isikae mtu. Wapiga vita wa Babeli wameacha kwenda vitani, hukaa ngomeni, nguvu zao zimezimia, wakageuka kuwa wanawake; makao yao ya mjini wameyateketeza, makomeo yao yakavunjwa. Mkimbizi anamfuata mkimbizi mwenziwe, vilevile mjumbe anamfuata mjumbe mwenziwe kumpasha mfalme wa Babeli habari, ya kuwa mji wake umetekwa, wakiutokea pande zote; ya kuwa vivuko vyote vimechukuliwa, ya kuwa manyasi ya bwawani yamechomwa moto, kwa hiyo wapiga vita wakaishia ukali. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Binti Babeli anafanana na mahali pa kupigia ngano pakitengenezwa na kupondwa, siku za mavuno zitaujia bado kidogo. Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, amenila, amenitowesha, ameniweka kuwa chombo kitupu, amenimeza kama joka na kulijaza tumbo lake, akanifukuza katika paradiso yetu. Makorofi, waliyonitendea, nayo miili ya watu, waliowaua kwetu, na iujie Babeli! ndivyo, watakavyosema wakaao Sioni; damu, walizozimwaga kwetu, na ziwajie wakaao katika nchi ya Wakasidi! ndivyo, watakavyosema Wayerusalemu. Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa hiyo mtaniona, nikiwagombea magomvi yenu, nikiwalipizia malipizi yenu; nitaukausha mto wao mkubwa, navyo visima vyao nitavinyima maji, vipwe. Hivyo Babeli utageuka kuwa machungu ya mabomoko na makao ya mbwa wa mwitu, kwa kustukiwa utazomelewa, kwa kuwa hautakaa mtu. Watanguruma wote pamoja kama simba, wataguna kama simba wachanga. Lakini vichwa vyao vitakapokuwa vinene, ndipo, nitakapowapa vinywaji vyao vya kuwalevya, wapige vigelegele, kisha walale usingizi wa kale na kale, wasiamke tena; ndivyo, asemavyo Bwana. Nitawaangusha kama wana kondoo, wakichinjwa kama madume ya kondoo na ya mbuzi. Kumbe Sesaki umetekwa! Kumbe umechukuliwa uliosifiwa na nchi zote! Kumbe Babeli umegeuka kuwa stusho kwa mataifa! Bahari imepanda kuja Babeli, ukafunikizwa na mawimbi yake yaumukayo. Miji yake ikawa ya kustukiwa kwa kuwa nchi kavu na jangwa, ni nchi isiyokaa mtu ye yote, wala hapapiti mwana wa mtu. Nitampatiliza naye Beli mle Babeli nikitoa kinywani mwake, aliyoyameza, mataifa yasimjie tena mengi na mengi; nazo kuta za boma la Babeli zitaanguka. Tokeni mwake, ninyi mlio ukoo wangu! Kila mtu na aiponye roho yake, asifikiwe na makali yake Bwana yenye moto! Mioyo yenu isizimie kwa woga, mtakapozisikia zile habari zitakazosikilika katika nchi hii, mwaka mmoja ikija habari, mwaka mwingine ikija habari tena, nao ukorofi ukizidi katika nchi hii, kwa kuwa watawala nchi watainukiana. Kwa hiyo mtaona, siku ikija, nitakapovipatiliza vinyago vya Babeli, nchi yake yote ipatwe na soni, kwa kuwa watu wake wote waliouawa wataanguka mlemle mwake. Ndipo, mbingu na nchi navyo vyote vilivyomo vitakapouzomea Babeli, kwani toka kaskazini waangamizaji wataujia; ndivyo, asemavyo Bwana. Babeli nao utaanguka kwa ajili ya Waisiraeli walioanguka wakiuawa, kama walivyoanguka watu wa nchi zote wakiuawa kwa ajili ya Babeli. Ninyi mliozikimbia panga, nendeni tu msisimame! Nako katika nchi za mbali mkumbukeni Bwana! Nao Yerusalemu na uingie mioyoni mwenu! Tuliona soni, tulipotukanwa, nyuso zetu zote zikaiva kabisa, wageni walipopaingia Patakatifu pa Nyumba ya Bwana. Ndivyo, asemavyo Bwana: Kwa hiyo mtaona, siku zikija, nitakapovipatiliza vinyago vyake Babeli; ndipo, wenye kuumizwa watakapopiga kite katika nchi yake yote. Babeli ingawa upande hata mbinguni kujijengea huko juu ngome yenye nguvu, huko nako waangamizaji wataujia; ndivyo, asemavyo Bwana. Sauti za makelele zinasikilika upande wa Babeli na shindo la vunjiko kubwa upande wa nchi ya Wakasidi. Kwani Bwana anauangamiza Babeli na kuzikomesha sauti za makelele yake makuu; mawimbi yanayoujia yanavuma kama maji mengi, sauti za kuumuka kwao zinazidi. Kwani mwangamizaji ameujia Babeli, wapiga vita wake watekwe, pindi zao zivunjwe, kwani Bwana ni Mungu mwenye lipizi, hulipisha, naye hasazi akilipisha. Ndipo, nitakapowalevya wakuu wake na werevu wake wa kweli na watawala nchi wake na wajumbe wake na wapiga vita wake, walale usingizi wa kale na kale, wasiamke tena; ndivyo, asemavyo Mfalme, Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake. Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kuta za boma la Babeli, zingawa ni nene, zitabomolewa mpaka chini, nayo malango yake, yangawa ni marefu, yatateketezwa kwa moto. Koo za watu husumbukia mambo ya bure, nayo makabila hujichokesha kwa ajili ya moto. Hili ndilo neno, mfumbuaji Yeremia alilomwagizia Seraya, mwana wa Neria, mwana wa Masea, alipokwenda Babeli pamoja na mfalme Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa ufalme wake; naye Seraya alikuwa mkuu wa makambi. Yeremia alikuwa ameyaandika hayo mabaya yote yatakayoujia Babeli katika kitabu kimoja, ni hayo maneno yote, Babeli uliyoandikiwa humo. Yeremia akamwambia Seraya: Utakapofika Babeli, jitafutie pafaapo, kisha yasome hayo maneno yote! Ndipo, utakaposema: Wewe Bwana, umepaambia mahali hapa, ya kuwa utapaangamiza, pasiwe mtu wala nyama atakayekaa hapa, kwani patakuwa peke yake tu kale na kale. Utakapokwisha kukisoma kitabu hicho, ukifungie jiwe, kisha ukitupe katikati katika mto wa Furati ukisema: Hivi ndivyo, Babeli utakavyozama, usioneke tena kwa ajili ya mabaya, mimi nitakayouletea, hata wazimie. Mpaka hapa ni maneno ya Yeremia. Sekedia alikuwa mwenye miaka 21 alipopata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 11; jina la mama yake ni Hamutali, binti Yeremia, wa Libuna. Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kama yote, Yoyakimu aliyoyafanya. Kwa kuwa Bwana aliwakasirikia Wayerusalemu na Wayuda, akawatupa, waondoke usoni pake, ikawa hivyo: Sedekia akakataa kumtii mfalme wa Babeli. Ikawa katika mwaka wa 9 wa ufalme wake mwezi wa kumi siku ya kumi ya mwezi, ndipo, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alipoujia Yerusalemu yeye na vikosi vyake vyote, wakapiga makambi huko, wakaujengea boma la kuuzungusha. Mji ukaja kusongwa hivyo na kuzingwa mpaka mwaka wa 11 wa mfalme Sedekia. Katika mwezi wa nne siku ya tisa njaa ikazidi mle mjini, watu wa nchi hii hawakuwa na vyakula. Ndipo, mji ulipobomolewa, nao wapiga vita wote wakatoroka na kutoka mjini na usiku kwa njia ya lango lililokuwa kati ya kuta mbili penye bustani ya mfalme; Wakasidi walipokuwa wamelala usingizi na kuuzunguka mji, wale wakashika njia ya nyikani. Kisha vikosi vya Wakasidi vikamfuata mfalme na kupiga mbio, vikampata Sedekia katika nyika ya Yeriko, navyo vikosi vyake vyote vilikuwa vimetawanyika na kumwacha. Wakamkamata mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribula katika nchi ya Hamati, akasema naye na kumhukumu. Mfalme wa Babeli akawaua wana wa Sedekia machoni pake, nao wakuu wote wa Wayuda akawaua huko Ribula. Kisha akayapofua macho yake Sedekia, akamfunga kwa minyororo; kisha mfalme wa Babeli akampeleka Babeli, akamtia kifungoni mpaka siku ya kufa kwake. Katika mwezi wa tano siku ya kumi ya mwezi, - ulikuwa mwaka wa 19 wa mfalme Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, - ndipo, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, aliyesimama usoni pa mfalme wa Babeli, alipoingia Yerusalemu. Akaiteketeza Nyumba ya Bwana na nyumba ya mfalme, nazo nyumba zote za Yerusalemu, nazo nyumba kubwa zote akaziteketeza kwa moto. Kisha vikosi vyote vya Wakasidi waliokuwa na mkuu wao waliomlinda mfalme vikazibomoa kuta za boma lililouzunguka Yerusalemu. Kisha Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawateka na kuwahamisha wanyonge wa ukoo huo nayo masao ya watu waliosalia mjini nao waliokuwa wamemwangukia mfalme wa Babeli na kurudi upande wake nao mafundi waliosalia. Lakini kwa wanyonge wa nchi Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, wengine akawasaza, waiangalie mizabibu, wengine walime tu. Lakini zile nguzo mbili za shaba zilizokuwa penye Nyumba ya Bwana na vile vilingo vya kuwekea mitungi ya maji na bahari ya shaba iliyokuwa penye Nyumba ya Bwana Wakasidi wakazivunja, nazo zile shaba zao zote wakazipeleka Babeli. Hata masufuria na majembe na makato ya kusafishia mishumaa na vyano na kata navyo vyombo vyote pia vya shaba vilivyotumiwa Nyumbani mwa Bwana wakavichukua. Nazo sahani na mikungu na mabakuli na vyano na taa na vijiko na vivukizio vilivyokuwa vya dhahabu tupu navyo vilivyokuwa vya fedha tupu mkuu wao waliomlinda mfalme akavichukua. Zile nguzo mbili na ile bahari moja na zile ng'ombe kumi na mbili zilizokuwa chini yake na vile vilingo vya kuwekea mitungi ya maji, ambavyo mfalme Salomo alivitengenezea Nyumba ya Bwana, shaba zao hivyo vyombo vyote hazikuwezekana kupimwa kwa mizani. Zile nguzo urefu wake nguzo moja ulikuwa mikono kumi na nane, nayo kamba ya mikono kumi na miwili ikaizunguka, unene wa shaba ulikuwa nyanda nne, ndani palikuwa penye uvurungu. Juu yake palikuwa na kilemba cha shaba, urefu wa kwenda juu wa hiki kilemba kimoja ulikuwa mikono mitano; hiki kilemba kilikuwa kimezungukwa na misuko kama ya mkeka iliyokuwa yenye komamanga, yote pia ni ya shaba; nayo nguzo ya pili ilikuwa vivyo hivyo, nayo ilikuwa yenye komamanga. Komamanga zilikuwa tisini na sita zilizoning'inia; komamanga zote penye msuko wa nguzo moja zilikuwa mia. Mkuu wao waliomlinda mfalme akamchukua mtambikaji mkuu Seraya na mtambikaji wa pili Sefania nao walinda kizingiti watatu. Namo mjini akachukua mtumishi mmoja wa nyumbani mwa mfalme aliyewekwa kuwa mkuu wa kuwasimamia wapiga vita na watu saba waliokuwa na kazi machoni pa mfalme waliopatikana mjini na mwandishi wa mkuu wa vikosi aliyewaandika watu wa nchi waliotakiwa uaskari na watu sitini wa shambani waliopatikana mle mjini. Hao akawachukua Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawapeleka Ribula kwa mfalme wa Babeli. Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribula katika nchi ya Hamati. Kisha akawahamisha Wayuda, waitoke nchi yao. Watu wa ukoo huu, Nebukadinesari aliowahamisha katika mwaka wa saba, ndio hawa: Wayuda 3023. Katika mwaka wa kumi na nane wa ufalme wa Nebukadinesari waliohamishwa Yerusalemu ni 832. Katika mwaka wa ishirini na tatu wa ufalme wa Nebukadinesari, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akahamisha Wayuda 745; wote pamoja walikuwa 4600. Ikawa katika mwaka wa 37 wa kuhamishwa kwake Yoyakini, mfalme wa Wayuda, katika mwezi wa kumi na mbili siku ya ishirini na tano, ndipo, Ewili-Merodaki, mfalme wa Babeli, alipomwonea uchungu Yoyakini, mfalme wa Wayuda; ikawa katika mwaka huohuo, alipoupata ufalme, akamtoa kifungoni, akasema naye maneno mema, akampa kiti chake cha kifalme juu ya viti vya kifalme vya wafalme wengine waliokuwa naye huko Babeli. Ndipo, alipoyavua mavazi yake ya kifungoni, akala chakula usoni pa mfalme pasipo kukoma siku zote, alizokuwapo. Nazo mali za kujitunza kila siku akapewa na mfalme wa Babeli siku zote, alizokuwapo, akapata siku kwa siku yaliyompasa mpaka siku ya kufa kwake. Kumbe uliokuwa mji wenye watu wengi unakaa peke yake! Uliokuwa mkuu katika wamizimu ukawa kama mjane! Uliokuwa mfalme wa kike wa miji unatumikishwa! Unalia usiku kucha, machozi yake yako mashavuni pake! Hakuna autulizaye moyo kwao wote walioupenda, wenziwe wote wakauacha kwa udanganyifu, wakawa adui zake. Wayuda wametekwa, wakapatwa na wasiwasi na utumishi mwingi; wanakaa kwenye wamizimu pasipo kuona kituo, wote waliowakimbiza wakawapatia mahali pa kubanana. Njia za Sioni zinasikitika, kwani hakuna wajao kula sikukuu, malango yake yote yako peke yao, watambikaji wake wanapiga kite, wanawali wake wametiwa majonzi, nao wanayaona kuwa machungu. Wausongao wako juu, adui zake wanafanikiwa, kwani Bwana ameutia majonzi kwa ajili ya mapotovu yake mengi, wachanga wake wakatekwa na kuhamishwa mbele yao wawasongao. Utukufu wake wote umemtoka yeye binti Sioni, wakuu wake wakawa kama kulungu wasioona malisho, wakaenda pasipo nguvu mbele yao wawakimbizao. Siku hizi za ukiwa na za kutangatanga Yerusalemu unayakumbuka mema yake yote yaliyoupendeza, ambayo ulikuwa nayo siku za kale. Watu wake walipotiwa mkononi mwake aliyewasonga, mwenye kuwasaidia hakuwako kabisa; waliowasonga walipoviona, wakacheka, jinsi walivyokomeshwa Yerusalemu umekosa kweli, kwa hiyo ukawa tapisho, wote walioutukuza wakaubeza, kwani waliuona, ulipokuwa uchi, nao unapiga kite kwa kurudi nyuma. Uchafu wake umezishika nguo zake ndefu, haukukumbuka mwisho kama huu; hivyo ulivyobwagwa chini unastaajaabisha, tena hakuna anayeutuliza moyo. E Bwana, utazame ukiwa wangu! Kwani adui wanajikuza. Mwenye kuusonga ameukunjua mkono wake, ayachukue mema yake yote yapendezayo; kwani aliona wamizimu, wakipaingia Patakatifu pake, nawe uliwakataza, wasipaingie penye mkutano wako! Watu wake wote wanapiga kite wakitafuta chakula, mema yao yapendezayo wanayanunua vilaji vya kujirudisha uzimani. Tazama, Bwana, uone, ya kuwa ninawaziwa kuwa si kitu! Je? Ninyi nyote mpitao njia, haviingii mioyoni mwenu? Chungulieni, mwone, kama yako maumivu yaliyo sawa nayo yangu yaliyonipata mimi, maana nimetiwa majonzi na Bwana, makali yalipomwaka moto. Toka juu akatuma moto kuiingia mifupa yangu, nao ukaishinda; miguu yangu akaitegea tanzi, akanirudisha nyuma, akanipa kuwa peke yangu, kwa hiyo ninaugua mchana kutwa. Mzigo wa mapotovu yangu ukafungwa kwa mkono wake, yaliposhikamana yakawekwa shingoni pangu; ndivyo, alivyozivunja nguvu zangu. Bwana akanitia mikononi mwao, ambao siwezi kuwainukia. Wanguvu wangu Bwana akawatupa wote, waondoke kwangu; akaita wengi, wanikusanyikie wawaponde wavulana wangu, mwanamwali binti Yuda Bwana akamkanyaga kamulioni. Kwa hiyo ninalia machozi, macho yangu mawili hutiririka maji, kwani mtuza moyo anikalia mbali, ndiye awezaye kuirudisha roho yangu. Watoto wangu wameachwa peke yao, kwani adui wanazidi nguvu. Sioni unainyosha mikono yake, lakini hakuna anayeutuliza moyo Bwana amewaagiza wamzungukao Yakobo, wamsonge tu; ndipo, Yerusalemu ulipowaziwa kwao kuwa si kitu. Lakini Bwana ni mwongofu, kwani nalikiinukia kinywa chake. Yasikieni, ninyi makabila yote, kayatazameni maumivu yangu! Wavulana na wasichana wangu wametekwa na kuhamishwa! Nikawaita walionipenda, lakini wakanidanganya. Watambikaji na wazee wangu wamezimia mijini walipojitafutia vyakula, wazirudishe roho zao. Tazama, Bwana! Kwani nimesongeka: matumbo yangu yamechafuka, moyo wangu nao humu kifuani umepinduliwa, kwa kuwa nalikataa kukutii kabisa. Nje upanga unawaua watoto, nyumbani huwa kama mwake kifo. Wakasikia, nilivyougua, lakini hakuna anitulizaye moyo, adui zangu wote walipoyasikia mabaya yaliyonipata, wakayafurahia, ya kuwa ndiyo, uliyoyafanya wewe. Utaileta ile siku, uliyoitangaza, ndipo, watakapokuwa kama mimi. Mabaya yao yote na yatokee usoni pako, uwafanyizie, kama ulivyonifanyizia kwa ajili ya mapotovu yangu yote! Kwani kupiga kite kwangu ni kwingi, nao moyo wangu huugua tu. Kumbe Bwana kwa makali yake anamkalisha binti Sioni chini! Utukufu wa Isiraeli uliofika hata mbinguni ameubwaga chini, alipokasirika hakukumbuka, ya kuwa ni pake pa kuiwekea miguu yake. Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo pasipo kuyaonea uchungu, kwa machafuko yake akayabomoa maboma ya binti Yuda, mfalme nao wakuu wake akawakumba, waanguke, kisha akawachafua. Makali yake yalipowaka moto, ndipo, alipokata pembe zote za Isiraeli, akaurudisha nyuma mkono wake wa kuume, uondoke usoni pa adui, akachoma moto kwake Yakobo, ukawa wenye miali iliyokula po pote. Akaupinda upindi wake, akawa kama adui, akajipanga na kuutumia mkono wake wa kuume, kama mwenye kusonga, akawaua wote walipendeza macho; hemani mwake binti Sioni ndimo, alimoyaeneza makali yake kama moto. Bwana akawa kama adui, alipommeza Isiraeli, akayameza majumba yake, akayaangamiza maboma yake, akamfurikishia binti Yuda kupiga kite na kuugua. Akakivunja kitalu chake kama cha bustanini, akauangamiza ua wake uliokuwa wa kukusanyikia; kisha Bwana akawasahaulisha Wasioni sikukuu nazo za mapumziko, akamtupa mfalame na mtambikaji, makali yake yalipowapatiliza. Pake pa kutambikiwa Bwana akapaona kuwa pabaya, napo Patakatifu pake, akapaacha. Akazitia mikononi mwa adui kuta za majumba yake, wakapiga makelele Nyumbani mwa Bwana kama yale ya sikukuu. Bwana amewaza moyoni kuziangamiza kuta za binti Sioni, akapapitisha kamba ya kupimia, hakuurudisha mkono, usipatoweshe, akalisikitisha boma pamoja na kuta zake, sasa zinatia uchungu. Malango yake yamezama, yamo mchangani ndani, makomeo yake akayaharibu kwa kuyavunja. Mfalme wake pamoja na wakuu wako kwa wamizimu, huko hawasikii, Maonyo yakisomwa, wala wafumbuaji wake hawafumbuliwi maono naye Bwana. Wazee wake binti Sioni hukaa chini na kunyamaza kimya, hujitupia mavumbi vichwani na kujifunga magunia, wanawali wa Yerusalemu huvielekeza vichwa vyao chini. Macho yangu yamezimia kwa kulia machozi, matumbo yangu nayo huchafuka; maini yangu yamemwagika chini kwa ajili ya mavunjiko yao walio wazaliwa wa ukoo wangu, kwani wachanga na wanyonyaji huzimia roho barabarani mjini. Nao huwauliza mama zao: Mikate na mvinyo iko wapi? wanapozimia barabarani mjini kama wenye kupigwa kwa panga, au wanapokata roho vifuani kwa mama zao. Nikutolee ushuhuda gani? Nikufananishe na nini, binti Yerusalemu? Nikulinganishe na nini, nikutulize moyo, mwanamwali binti Sioni? Kwani vunjiko lako ni kubwa kama bahari, atakayekuponya ni nani? Wafumbuaji wako waliyoyaona yalikuwa uwongo na upumbavu, hawakuyafunua maovu yako, uliyoyafanya, wayafungue mafungo yako, ila walipokuambia: Tumeona, yalikuwa uwongo, wakupatie kutekwa. Wote wapitao njiani wanakupigia makofi, hukuzomea, binti Yerusalemu, wakivitingisha vichwa vyao, kwamba: Je? Huu ni ule mji, watu waliouita: Timilizo la uzuri, tena: Furaha ya nchi zote? Adui zako wote wakaviasama vinywa vyao, wakakuzomea wakikukerezea meno na kusema: Tumemmeza! Hii ni siku, tuliyoingojea, tumeipata, tumeiona! Bwana ameyafanya aliyoyawaza, akalitimiza neno lake, aliliagiza tangu siku za kale, akabomoa pasipo kuona uchungu, adui zako wakakufurahia, alipozikuza pembe zao waliokusonga Mioyo yao ikamlilia Bwana: Ninyi kuta za binti Sioni, churuzisheni machozi mchana na usiku kama ni mto! Usijipatie pumziko! Mboni ya jicho lako isinyamaze! Inuka, ulie usiku kucha, zamu za usiku zikipokeana! Umwage moyo wako, kama ni maji mbele ya uso wake Bwana! Mnyoshee mikono yako kwa ajili ya roho za watoto wako wachanga wanaozimia kwa njaa po pote barabarani pembeni! E Bwana, tazama, uone! Ni nani, uliyemfanyizia hivyo? Je? Wanawake wayale mazao yao, watoto wao waliolelewa nao? Je? Watambikaji na wafumbuaji wauawe Patakatifu pake Bwana? Wana wa wazee hulala barabarani chini, wasichana na wavulana wangu wameuawa kwa panga; umewaua siku ile, makali yako yalipotokea, ukawachinja pande zote pasipo kuwaonea uchungu! Ukawaita wote walionitia woga, watoke pande zote, kama ni siku ya mkutano, lakini ilikuwa siku ya makali ya Bwana, napo hapo hawakuwako walioona pa kuponea wala pa kukimbilia, nao, niliowalea na kuwakuza, adui wakawamaliza. Mimi ni mtu wa kiume, lakini niliteseka nilipopigwa fimbo yenye machafuko yake. Akaniongoza na kuniendesha, nije gizani, nisije mwangani. Ananirudia mimi peke yangu, mkono wake ukinigeukia mchana kutwa. Akazinyausha nyama na ngozi za mwili wangu mimi, mifupa yangu yote akaivunja nayo. Akanizibia njia akanizungushia mambo yenye sumu na usumbufu. Akanikalisha penye giza kuu kama waliokufa kale. Ukuta unanizunguka, nisitoke, akanifunga minyororo mizito. Ijapo nilie na kupiga yowe, maombo yangu huyazibia masikio. Akazifunga njia zangu kwa mawe yaliyochongwa, napo pengine, nilipopita, akapafanya, pasipitike tena. Yeye akaniwia kama nyegere aoteaye au kama simba aliomo mafichoni. Njia zangu akazipoteza, akaninyafua, akaniweka mahali palipo peke yake. Akaupinda upindi wake, akanitumia kuwa shabaha ya kuipiga mishale. Iliyokuwa podoni mwake akaipiga, inichome mafigo Nikawa kicheko kwao wote walio ukoo wangu, wakanizomea mchana kutwa. Akanishibisha kwa kunilisha yaumizayo matumbo, akaninywesha maji machungu. Akayakerezesha meno yangu na kuyaumisha vijiwe, akanigaagaza majivuni. Ukaifukuza roho yangu, isipate kutulia, nikasahau kulivyo, mtu akikaa vema. Nikasema: Nguvu zangu zimepotea pamoja na kingojeo changu cha kumngojea Bwana. Ukumbuke ukiwa wangu na wasiwasi wangu, nikilishwa machungu, nikinyweshwa yenye sumu! Roho yangu haiachi kuyakumbuka, kwa kuwa imeinamishwa humu ndani yangu. Haya na niyaweke moyoni tena, ndivyo, nitakavyopata kumngojea: *Ni upole wake Bwana, tusipomalizika, kwani huruma zake hazikuisha, kila kunapokucha ni mpaya, nao walekevu wake ni mwingi. Fungu langu ni Bwana! ndivyo, roho yangu isemavyo: kwa hiyo nitamngojea. Bwana huwawia mwema wamngojeao nao wamtafutao kwa roho. Inafaa kuvumilia na kuungojea wokovu wa Bwana. inamfalia mtu wa kiume, akitwikwa mizigo akingali kijana bado. Na akae peke yake na kunyamaza kimya, kwani Bwana ndiye aliyemtwika. kinywa chake akiweke uvumbini, kwani labda liko la kulingojea. Ampigaye na amgeuzie shavu, na ashibe matusi. Bwana hamtupi mtu kale na kale. Bwana akimtia mtu majonzi atamhurumia tena, kwani upole wake ni mwingi.* Kwani siko kupenda kwa moyo wake, akiwaumiza wana wa watu na kuwapiga. Mtu akiwaponda na kuwapiga mateke kwa miguu wote waliofungwa huku nchini, au mtu akimpotoa mwenziwe na kumnyima yampasayo usoni pake Alioko huko juu, au mtu akimgeuza mwenziwe mkweli shaurini kuwa mwongo, Bwana asiyatazame? Yuko nani awezaye kusema neno, likawapo, Bwana asipoliagiza? Je? Yeye Alioko huko juu aliyoyasema, hayatokei yakiwa mabaya au yakiwa mema? Mtu hununia nini siku zote za kuwapo? Kila mtu na ayanunie makosa yake! Na tuzijaribu njia zetu na kuzichunguza, tupate kurudi upande wake Bwana! Na tumwinulie Mungu mbinguni mioyo yetu pamoja na mikono yetu! Sisi ndio tuliokosa tusipokutii, nawe hukutuondolea. Ulipojivika makali ulitukimbiza, ukaua pasipo huruma. Ukajivika wingu, likufunike, malalamiko yasikufikie. Ukatufanya kuwa takataka za kutupwa tu katikati ya makabila ya watu. Wakatuasamia vinywa vyao wote waliokuwa adui zetu. Yaliyotupata yalikuwa mastuko na mashimo na maangamizo na mavunjiko. Macho yangu huchuruzika vijito vya maji kwa ajili ya mavunjiko yao walio wazaliwa wa ukoo wangu. Macho yangu hulia machozi pasipo kupumzika, hayakomeki, mpaka Bwana achungulie toka mbinguni, ayaone. Macho yangu huniumiza roho kwa kuona, wanawake wote wa mji wangu walivyo. Kweli wameniwinda kama ndege wale wanichukiao bure tu; wakanitupa shimoni, wanizimishe roho, wakanitupia mawe. Maji yenye nguvu yakakididimiza kichwa changu, nikasema: Basi, nimekatwa roho. nikalililia Jina lako, Bwana, nilipokuwa shimoni kuzimuni. Ukaisikia sauti yangu nilipokuomba: Usiyazibe masikio yako, nikikupigia kite na kukuomba wokovu. Ukanijia karibu siku ile, nilipokulilia, ukaniambia: Usiogope! Ukanigombea magomvi ya roho yangu ukanikomboa na kunirudisha uzimani. Ukaona, Bwana, jinsi nilivyopotolewa, ukayakata mashauri yangu. Ukayaona yote, waliyoyataka kunilipizia, nayo yote, waliyoyawaza ya kunifanyizia. Ukayasikia, Bwana, matusi yao nayo yote, waliyoniwazia. Ukayasikia, waniinukiao waliyoyasema wakinipigia mashauri mchana kutwa. Tazama, uone! Ikiwa wanakaa, au ikiwa wanasimama: mimi ndiye, wanayemzomea. Uwalipishe, Bwana, matendo yao ukiwafanyizia, kama mikono yao ilivyofanya! Uwashupaze mioyo yao, apizo lako likiwajia! Uwakimbize kwa makali yako na kuwaangamiza, watoweke chini ya mbingu za Bwana! Imekuwaje, dhahabu ikichujuka, dhahabu iliyo nzuri yenyewe ikigeuka kuwa mbaya? Imekuwaje, vijiwe vya pambo vya Patakatifu vikitupwa pembeni penye barabara zote? Vijana wa Sioni waliohesabiwa kuwa mali, waliolinganishwa na dhahabu tupu, imekuwaje, wakiwaziwa kuwa vyombo vya udongo vinavyofanywa kwa mikono ya mfinyanzi? Mbwa wa mwitu nao hutoa maziwa ya kuwanyonyesha watoto wao, lakini wanawake wao walio ukoo wangu wamegeuka, wasione uchungu kama mbuni wa nyikani. Ndimi za vitoto vinyonyavyo zinagandamana na fizi zao kwa kiu; wana wachanga wanaomba mkate, lakini hakuna anayewamegea. Waliokula vya urembo wanazimia barabarani kwa njaa, waliokuzwa na kuvikwa mavazi mororo ya kifalme sasa wanalala jaani. Manza, walizozikora wazaliwa wa ukoo wangu, ni kubwa kuliko makosa ya Sodomu uliogeuzwa kwa kitambo kimoja kuwa si mji tena, lakini haikuwako mikono ya watu iliyougusa tu. Wakuu wao waling'aa kuliko theluji, wakawa weupe kuliko maziwa; miili yao ilikuwa miekundu kuliko marijani, sura zao zilikuwa kama za jiwe la safiro; lakini sasa ukiwatazama, ni weusi kuliko masizi, hawajulikani barabarani, ngozi zao zimekunjana na kugandamana na mifupa yao, zimekauka, zikawa kama maganda ya mti. Waliouawa kwa panga ndio waliopata mema, kuliko wao waliouawa kwa njaa; hao ndio waliozimia wakichomwa na ukosefu wa mazao ya mashamba. Ikawa, wanawake wenye uchungu wakawatokosa wana wao wenyewe kwa mikono yao, wawe chakula chao hapo, wazaliwa wa ukoo wangu walipovunjwa. Bwana ameyatimiza machafuko yake, akayamwaga makali yake yenye moto; hivyo ndivyo, alivyowasha moto Sioni ulioila nayo misingi yake. Wafalme wa nchi nao wote wakaao humu ulimwenguni kwao hakuwako aliyeitikia kwamba: Malangoni mwa Yerusalemu ataingia ausongaye au adui ye yote. Hayo yamefanyika kwa ajili ya makosa ya wafumbuaji wake na kwa ajili ya maovu, watambikaji waliyoyafanya walipomwaga mwake katikati damu zao waliokuwa waongofu. Wakatangatanga barabarani kama vipofu, kwa kuwa walijichafua kwa damu, watu wasiweze kabisa kuzigusa nguo zao. Mwondokeeni mchafu! Ndivyo, watu walivyotangaza mbele yao. Ondokeni! Ondokeni! Msiwaguse! Walipopiga mbio na kutangatanga hivyo, watu wakasema nako kwa wamizimu: Wasikae tena kuwa wageni wetu! Macho ya Bwana yenye ukali yakawatenga, naye hatawatazama tena; kwani hawakuwaheshimu watambikaji, wala wazee hawakuwahurumia. Nasi macho yetu yakafifia yasipokoma kuutazamia msaada wetu, lakini haukupatikana; katika kilindo chetu tukaendelea kuchungulia taifa, lakini halikuwako lililoweza kutuokoa. Wakazinyatia nyayo zetu, tusiweze kwenda katika barabara zetu; mwisho wetu uko karibu, siku zetu zimetimia, kwani mwisho wetu umefika. Watukimbizao ni wepesi kuliko tai wa mbinguni, wakatufukuza nako milimani juu na kutuvizia nyikani. Aliyekuwa kama pumzi puani mwetu yeye aliyepakwa mafuta na Bwana akanaswa katika mashimo yao; ni yeye, tuliyemsema: Kivulini kwake tutakaa kwenye makabila ya watu Furahi na kujichekelea, binti Edomu, ukaaye katika nchi ya Usi! Wewe nawe kitakufikia hiki kinyweo, ulewe, mpaka ujikalishe mwenye uchi. Manza, ulizozikora, binti Sioni, zimemalizika: Bwana hatakutoa tena, uhamishwe. Manza, ulizozikora, binti Edomu, atakupatilizia atakapoyavumbua makosa yako. Bwana, yakumbuke yaliyotupata! Tazama, uone, jinsi tunavyotiwa soni! Mafungu yetu ya nchi yamechukuliwa, yawe mali za wengine, nyumba zetu zinakaa wageni. Tumegeuka kuwa wana waliofiwa na baba zao, mama zetu ni kama wajane. Maji yetu tunayanywa tukiyanunua kwa fedha, kuni zetu nazo tunazipata tu tukizilipa. Watukimbizao wako penye shingo zetu; tunapochoka hatuoni pa kupumzika. Wamisri na Waasuri tukawanyoshea mikono, tupate vyakula vya kushiba. Baba zetu waliokosa hawako tena, nasi tunatwikwa manza, walizozikora wao. Watumwa ndio wanaotutawala, lakini hakuna anayetupokonya mikononi mwao. Tunaziponza roho zetu tukijichumia vyakula, kwa kuwa nako nyikani ziko panga. Ngozi zetu ni zenye moto kama wa tanuru kwa kuteketezwa na njaa. Wanawake waliokuwamo Sioni waliwakorofisha, nao wasichana waliokuwako katika nchi za Yuda. Wakuu wakanyongwa kwa mikono yao, nazo nyuso za wazee hazikupewa macheo. Vijana hutwikwa majiwe ya kusagia, watoto huvunjwa na mizigo ya kuni. Ndipo, wazee walipoyaacha maongezi ya malangoni, nao vijana wakayakomesha mazeze yao. Yakakoma yaliyoifurahisha mioyo yetu, michezo yetu ya ngoma ikageuka kuwa maombolezo. Vilemba vilivyovipamba vichwa vyetu vimekwisha kuanguka chini, tukapatwa na mabaya, kwa kuwa tumekosa. Kwa hiyo mioyo yetu imezimia, kwa hiyo macho yetu nayo yameguiwa na giza. Ni kwa ajili ya mlima wa Sioni ulioko peke yake, kwa kuwa ni mbweha tu wanaotembea huko. Wewe Bwana, unakaa kale na kale, kiti chako cha kifalme kiko kwa vizazi na vizazi! Mbona unatusahau kale na kale, ukatuacha siku hizi zilizo nyingi? Bwana, turudishe kwako! Ndivyo, tutakavyopata kurudi; siku zetu zigeuke kuwa mpya tena kama zile zilizopita! Kweli umetutupa kabisa, umetukasirikia sanasana. Ikawa siku ya tano ya mwezi wa nne katika mwaka wa 30, nilipokuwa katikati ya mateka waliohamishwa kwenye mto wa Kebari, ndipo, mbingu zilipofunuka, nikaona maono ya Mungu. Siku hiyo ya tano ya mwezi huo ilikuwa ya mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yoyakini. Ndipo, neno la Bwana lilipomjia Ezekieli, mwana wa Buzi; naye alikuwa mtambikaji katika nchi ya Wakasidi kwenye mto wa Kebari, nao mkono wake Bwana ulikuwa juu yake. Nilipotazama nikaona upepo wenye nguvu uliotoka kaskazini na wingu kubwa lililowaka mioto iliyokamatana na kumetameta po pote, namo ndani yake mlikuwamo kilichofanana na shaba iliyong'aa sana mle motoni katikati. Humo ndani katikati mkaonekana yaliyokuwa kama nyama wanne, nao nilipozitazama sura zao, zilikuwa kama mifano ya mtu. Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, tena kila mmoja alikuwa na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyoka, lakini nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za ndama, zikametuka kama shaba iliyokatuliwa sana. Chini ya mabawa yao kulikuwa na mikono ya kimtu pande zote nne. Nyuso zao na mabawa yao hao wanne yalikuwa hivyo: mabawa yao yalikuwa yanashikana kila moja na bawa lenziwe; nao walipokwenda hawakuzigeuza nyuso zao, ila kila mmoja alikwenda na kufuata hapo, uso wake ulipoelekea. Nyuso zao mifano yao ilikuwa hivyo: mbele ni uso wa mtu, kuumeni kwao hao wanne ni uso wa simba, kushotoni kwao hao wanne ni uso wa ng'ombe, tena kwao hao wanne nyuma yao ni uso wa tai. Nayo mabawa yao yalikuwa yamejitanda juu, kwake kila mmoja mawili yalishikana, mawili yaliifunika miili yao. Kila mmoja wakaenda na kufuata hapo, uso wake lulipowlekea; roho zao zilikotaka kwenda, ndiko, walikokwenda tu pasipo kuzigeuza nyuso. Nazo sura za hao nyama nilipozitazama, zilifanana kuwa kama makaa ya moto yaliyowaka kwa mfano wa mienge iliyokwenda huko na huko katikati yao hao nyama, nao moto huo ulikuwa umeng'aa kabisa, hata umeme ulitoka humo motoni. Kisha hao nyama wakapiga mbio kwenda na kurudi, vikaonekana kuwa kama umeme. Nilipowatazama hao nyama mara nikaona gurudumu moja huku nchini kando yao hao nyama pande zote nne. Nilipoyatazama hayo magurudumu, jinsi yalivyotengenezwa, jinsi yalivyokuwa, yalikuwa kama kito cha Tarsisi, yote manne mfano wao ulikuwa huo mmoja; nilipoyatazama tena, jinsi yalivyotengenezwa, yalionekana kuwa kama gurudumu moja lililomo ndani ya gurudumu lenziwe. Yalipokwenda yalikwenda panda zote nne pasipo kugeuka katika mwendo wao wa kwenda mbele tu. Vikuku vyao vilikuwa virefu mno vya kuogopesha; tena hivi vikuku vilijaa macho po pote kwao yote manne. Wale nyama walipokwenda, hayo magurudumu yalikwenda nayo kando; tena hao nyama walipochukuliwa juu kutoka katika nchi, hayo magurudumu yakachukuliwa juu nayo. Roho zao hao zilikotaka kwenda, ndiko, walikokwenda; roho zao zilipotaka kwenda huko, nayo magurudumu yalichukuliwa kwenda pamoja nao, kwani roho za hao nyama zilikuwa namo katika magurudumu. Hao walipokwenda, nayo yalikwenda; hao waliposimama, nayo yalisimama; hao walipochukuliwa juu kutoka katika nchi, nayo magurudumu yalichukuliwa kwenda pamoja nao, kwani roho za hao nyama zilikuwa namo katika magurudumu. Juu ya vichwa vyao hao nyama kulikuwako lililofanana na ukingo, mfano wake ulikuwa kama ulanga uangazikao vizuri mno, mtu aogope kuutazama, nao ulikuwa umetandwa juu penye vichwa vyao. Chini ya huo ukingo mabawa yao yalikuwa yamenyoka, kila moja kikielekea lenziwe, kila nyama mmoja mabawa mawili yalikuwa ya kujifunikia juu, tena mabawa mawili yalikuwa ya kujifunikia miili yao. Nikazisikia sauti za mabawa yao, nazo zilikuwa kama sauti za maji mengi au kama shindo la Mwenyezi. Walipokwenda sauti za kuvuma zilikuwa kama za uvumi wa makambi ya vikosi vya askari. Waliposimama huyalegeza mabawa yao. Kisha waliposimama na kuyalegeza mabawa yao, kulikuwa na uvumi huko kwenye ukingo uliokuwa juu ya vichwa vyao. Tena juu ya ukingo uliokuwa juu ya vichwa vyao kulionekana kilichokuwa kama kito cha Safiro, nacho kilifanana na kiti cha kifalme; tena katika hicho kilichofanana na kiti cha kifalme kulionekana aliyefanana na mtu, anakikalia. Nilipotazama tena nikaona ndani yake kilichofanana na shaba iliyong'aa sana, kilionekana kuwa kama moto uliofungiwa nyumbani po pote. Tena hapo palipokuwa kama kiuno chake mpaka juu, tena toka hapo palipofanana kuwa kama kiuno chake mpaka chini nilipopatazama nikaona kuwa kama moto uung'aao kabisa po pote. Ulionekana kuwa kama upindi ulioko mawinguni siku ya mvua, ndivyo, kuangazika kwake kulivyokuwa po pote; huu ndio mfano wa utukufu wake Bwana. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mwenye kusema. Akaniambia: Wewe mwana wa mtu, simama kwa miguu yako, niseme na wewe! Aliposema na mimi, roho ikanijia, ikanipa kusimama kwa miguu yangu, nikamsikia aliyesema na mimi. Akaniambia: Wewe mwana wa mtu, mimi ninakutuma kwa wana wa Isiraeli walio mataifa makatavu, walionikataa mimi, wao wenyewe na baba zao wamenikosea mpaka leo. Hawa wana nao ni wenye nyuso zishupaazo na wenye mioyo migumu. Sasa mimi ninakutuma kwao, uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema! Nao ikiwa wanasikia, au ikiwa wanaacha kusikia, kwani ndio mlango mkatavu, lakini watajua, ya kuwa yuko mfumbuaji katikati yao. Nawe mwana wa mtu, usiwaogope! Wala maneno yao usiyaogope! Ijapo miiba ikuchome, ijapo ukae penye nge, usiyaogope maneno yao! Wala usizistuke nyuso zao! Kwani ndio mlango mkatavu. Sharti uwaambie maneno yangu, ikiwa wanasikia, au ikiwa wanaacha kusikia, kwani ndio wakatavu. Nawe mwana wa mtu, yasikie, mimi ninayokuambia! Usiwe mkatavu kama mlango huu mkatavu! Kifumbue kinywa chako, ule, mimi nitakachokupa! Nilipotazama nikaona mkono nilionyosewa mimi, namo mwake nikaona kitabu kilichozingwa. Akakizingua, nacho kilikuwa kimeandikwa upande wa mbele na wa nyuma; nayo yaliyoandikwa humo yalikuwa maombolezo na masikitiko na vilio. Akaniambia: Mwana wa mtu, utakachokiona, kile! Ukile kitabu hiki kilichozingwa! Kisha nenda kusema na mlango wa Isiraeli! Nikakifunua kinywa changu, akanilisha hicho kitabu cha kuzingwa. Akaniambia: Mwana wa mtu, lilishe tumbo lako, uyajaze matumbo yake hiki kitabu cha kuzingwa, mimi ninachokupa! Basi, nikakila, kikawa kitamu kinywani mwangu kama asali. Akaniambia: Mwana wa mtu, nenda, ufike kwao wa mlango wa Isiraeli, uwaambie niliyokuambia! Kwani wewe hutumwi kwa kabila lenye msemo mgumu na ndimi nzito, ila kwa mlango wa Isiraeli. Hutumwi kwa makabila mengi yenye misemo migeni na ndimi nzito, usizozisikia; kama ningekutuma kwao hao wangekusikia. Lakini hawa wa mlango wa Isiraeli watakataa kukusikia, kwani hawataki kunisika mimi, kwani mlango wote wa Isiraeli ndio wenye mapaji mashupavu na wenye mioyo migumu. Tazama: Nao uso wako nitaushupaza kuwa sawasawa kama zao, nalo paji lako nitalishupaza kuwa sawasawa kama yao. Kama almasi inavyoshupaa kuliko mwamba, ndivyo, nilivyolipa paji lako kuwa. Usiwaogope, wala usizistuke nyuso zao! Kwani ndio mlango mkatavu. Akaniambia: Mwana wa mtu, maneno yangu yote, nitakayokuambia, yaweke moyoni mwako ukiyasikia kwa masikio yako! Kisha nenda ufike kwao waliotekwa na kuhamishwa, walio wana wa ukoo wako, useme nao na kuwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema. Ikiwa wanasikia, au ikiwa wanaacha kusikia, basi. Upepo ukanichukua, nikasikia nyuma yangu sauti ya uvumi mkubwa wa kwamba: Utukufu wa Bwana na utukuzwe hapo, alipo! Kukasikilika nako kuvuma kwa mabawa ya wale nyama, wakigusana na kuvuma, na kuvuma kwa yale magurudumu yaliyokuwako kwao, zikawa sauti za uvumi mkubwa. Upepo ukanichukua, ukanipeleka; nami nikaenda kwa uchungu wa kukasirika rohoni mwangu, nao mkono wa Bwana ulikuwa ukinishika kwa nguvu. Hivyo ndivyo, nilivyokuja Teli-Abibu kwao waliotekwa na kuhamishwa, waliokaa kwenye mto wa Kebari; huko walikokaa hao, ndiko, nilikokaa nami siku saba nikiwa kimya katikati yao kwa kushangaa. Hizo siku saba zilipopita, neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, nimekuweka kuwa mlinzi wa mlango wa Isiraeli. Hapo, utakaposikia neno kinywani mwangu, sharti uwaonye, wanisikie. Ninapomwambia mtu asiyenicha: Utakufa, nawe usipomwonya, usiposema naye yeye asiyenicha, kwamba umwonye, aiache njia yake, umpatie kuwapo uzimani, basi, yeye asiyenicha atakufa kwa manza zake, alizozikora, lakini damu yake nitakulipisha, kwani itakuwa imeishika mikono yako. Lakini wewe unapomwonya asiyenicha, naye asipoyaacha mapotovu yake, asiporudi katika njia yake ipotokayo, basi, yeye atakufa kwa manza zake, alizozikora, nawe wewe utakuwa umeiokoa roho yako. Tena mwongofu anapouacha wongofu wake, afanye mapotovu, nitaweka mbele yake pa kujikwalia, naye atakufa. Ikiwa hukumwonya, atakufa kwa makosa yake, nayo maongofu yake, aliyoyafanya, hayatakumbukwa, lakini damu yake nitakulipisha, kwani itakuwa imeishika mikono yako. Lakini wewe unapomwonya mwongofu, asikose kwa kuwa mwongofu, naye akaacha kukosa, basi, atakaa uzimani, kwani ameonyeka, nawe utakuwa umeiokoa roho yako. Ndipo, mkono wa Bwana ulipokuja kuwa juu yangu, akaniambia: Ondoka kwenda kwenye mbuga iliyoko bondeni! Ndiko, nitakakosema na wewe. Nikaondoka kwenda kwenye mbuga iliyoko bondeni, mara nikauona utukufu wa Bwana, ukisimama hapo, ulikuwa kama ule utukufu, niliouona kwenye mto wa Kebari, nikaanguka kifudifudi. Kisha roho ikanijia, ikanipa kusimama kwa miguu yangu. Akasema na mimi, akaniambia: Ingia nyumbani mwako, ufungiwe humo! Nawe mwana wa mtu, utaona, wakikutia kamba, wakufunge nazo, usiweze kutoka katikati yao. Nao ulimi wako nitaugandamanisha na ufizi wako, uwe bubu, usiweze tena kuwaonya, kwani ndio mlango mkatavu. Lakini hapo, nitakaposema na wewe, nitakifumbua kinywa chako, uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema. Mwenye kusikia atasikia; lakini mwenye kukataa atakataa vilevile, kwani ndio mlango mkatavu. Wewe mwana wa mtu jipatie tofali, uliweke mbele yako! Kisha chora humo mji wa Yerusalemu! Kisha uuzungushie boma! Hilo boma ulijengee minara, ulizungushie hata ukingo wa mchanga! Tena uupigie po pote makambi ya askari, uweke nayo magogo ya kuvunjia boma! Kisha jipatie bati la chuma, kalisimamishe kuwa ukuta wa chuma wa kukutenga wewe nao mji! Kisha uuelekezee uso wako, kwamba uwe ukisongwa, nawe uwe mwenye kuusonga! Hiki ndicho kielekezo, mlango wa Isiraeli utakachokipata. Tena wewe ulalie ubavu wako wa kushoto, ukiisha ziweke manza za mlango wa Isiraeli juu yake; siku, utakazoulalia, zitahesabiwa kuwa siku za kuzichukua manza zao. Nami nitakupa miaka ya manza zao kuwa hesabu ya hizo siku, zitakuwa 390; ndizo, utakazozichukua manza za mlango wa Isiraeli. Utakapozimaliza hizo siku, uulalie ubavu wako wa kuume mara ya pili, uzichukue manza za mlango wa Yuda siku 40; kwa kila mwaka mmoja nimekupa siku moja. Tena uso wako utauelekezea Yerualemu uliosongwa, hata mkono wako, ukiisha kuuondoa nguo. Kisha sharti uufumbulie huo mji yatakayokuwa. Tena utaniona nikikufunga kwa kamba, usiweze kugeuka na kuulalia ubavu wa pili, mpaka uzimalize siku za kusongwa kwako. Tena jipatie ngano na mawele na maharagwe na choroko na mtama mweupe na mwekundu, uzitie zote katika chombo kimoja! Ndizo ujitengenezee mikate, kama hesabu ilivyo ya siku, utakazoulalia ubavu wako; siku 390 utaila hio mikate. Hicho chakula chako, utakachokila, utapimiwa kwa mizani kila siku ratli moja kaso robo muda kwa muda. Maji nayo utakunywa kwa kupimiwa, nusu kibaba kila siku moja, nayo utayanywa muda kwa muda. Hiyo mikate utaila, ikitengenezwa kama mikate ya mofa ya mawele, nawe sharti uichome kwa mavi ya choo cha mtu machoni pao. Bwana akasema: Kwenye mataifa, nitakakowatupa, wana wa Isiraeli, watavila vyakula vyao, vikiwa vichafu vivyo hivyo. Nikasema: E Bwana Mungu, tazama, roho yangu haijatiwa uchafu; tangu hapo, nilipokuwa mtoto, mpaka sasa sijala kibudu wala makombo ya nyama wa porini, wala yenye uvundo hayajaingia kinywani mwangu. Akaniambia: Tazama, nimekupa mavi ya ng'ombe penye mavi ya mtu, ndiyo utumie ya kuchomea mikate yako. Akaniambia: Mwana wa mtu, utaniona, nikilivunja shikizo la chakula mle Yerusalemu, wale vyakula vyao kwa kupimiwa na mizani na kwa kuvihangaikia; nayo maji watakunywa kwa kupimiwa na kwa kupigwa na bumbuazi, kwani watakosa vyakula na maji, wapigwe na bumbuazi wote pamoja, wakitoweshwa kwa ajili ya manza zao walizozikora. Nawe mwana wa mtu, jipatie upanga mkali, uutumie kuwa wembe wa kinyozi wa kunyolea kichwa chako na udevu wako! Kisha jipatie mizani, uzigawanye hizo nywele! Fungu la tatu uliteketeze kwa moto mjini katikati, siku za kusongwa zitakapomalizika! Fungu la tatu jingine lichukue, ulitapanye na kupigapiga kwa upanga ukizunguka mjini po pote! Nalo fungu la tatu jingine utalitupatupa kwenye upepo, nami nitauchomoa upanga, uzifuata nyuma. Nawe hizo nywele zichukue chache tu, uzifungue pembeni katika vazi lako! Namo uchukue tena kidogo, uzitupe penye ule moto unaowaka mjini katikati, uziteketeze mle motoni! Ndimo, utakamotoka moto wa kuula mlango wote wa Isiraeli. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Huu ndio Yerusalemu! Nimeuweka kwenye wamizimu katikati, ukazungukwa na nchi zao. Lakini kwa kuwa haukunicha, uliyakataa mashauri yangu kuliko hao wamizimu, ukayakataa nayo maongozi yangu kuliko hizo nchi ziuzungukazo, kwani mashauri yangu wakayabeua, hawakuyafuata maongozi yangu. Kwa sababu hii Bwana Mungu anasema hivi: Kwa kuwa mnafanya matata kuliko wamizimu wanaowazunguka, msipoyafuata maongozi yangu, wala msipoyafanya mashauri yangu, wala msipoyafanya maamuzi yangu, wamizimu wawazungukao wanayoyafanya, kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Utaniona, mimi nami nikikujia, nifanye katikati yako mashauri machoni pa wamizimu. Nitakufanyizia mambo, nisiyoyafanya bado, wala sitayafanya mara nyingine yaliyo hivyo kwa ajili ya machukizo yako yote. Nayo ni haya: katikati yako baba watakula wana, nao wana watakula baba zao! Haya ndiyo mashauri, nitakayokufanyizia, kisha masao yako nitayatupiatupia pande zote za upepo. Kweli ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo nilivyo Mwenye uzima, kwa kuwa umepachafua Patakatifu pangu kwa matapisho yako yote na kwa machukizo yako yote, kwa hiyo mimi nami nitaliondoa jicho langu, lisikuonee uchungu, nami mwenyewe sitakuhurumia. Fungu lako la tatu watakufa kwa magonjwa mabaya wakizimia kwa njaa katikati yako, fungu la tatu jingine watauawa kwa panga kwenye pande zako zote; fungu la tatu jingine nitawatupiatupia pande zote za upepo, kisha nitauchomoa upanga, uwafuate. Hivyo makali yangu yatakwisha, hivyo nitayapoza machafuko yangu yenye moto kwao nikiwalipisha. Ndipo, watakapotambua, ya kuwa mimi Bwana nimesema kwa wivu wangu, nikawatimilizia machafuko yangu yenye moto. Kisha nitakugeuza kuwa mabomoko ya kuzomelewa kwa wamizimu wote wakuzungukao, kila atakayepapita ayaone. Hivyo itakuwa, uwe wa kuzomelewa na wa kufyozwa, tena uwe kitisho cha kuwashangaza wamizimu wakuzungukao, nitakapokufanyizia mashauri na kukutolea makali na machafuko yenye moto na mapigo yenye moto. Mimi Bwana nimeyasema. Ndipo, nitakapowapigia mishale mibaya ya njaa ya kuangamiza; hiyo ndiyo, nitakayoipiga kweli, iwaangamize ninyi, nitakapoizidisha njaa na kulivunja kabis shikizo lenu la chakula. Pamoja na hiyo njaa nitawapelekea nyama wabaya, wawaue watoto wako, nayo magonjwa mabaya ya kuozesha damu yatapita kwako, kisha nitaleta nazo panga na kukuua. Mimi Bwana nimeyasema. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, ielekezee milima ya Isiraeli uso wako, uifumbulie yatakayokuwa! Useme: Milima ya Isiraeli, lisikieni neno la Bwana Mungu! Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema, mvisikie ninyi milima na vilima na vijito na mabonde: Mtaniona, nikileta panga kwenu, niyakomeshe matambiko yenu ya vilimani. Ndipo, penu pa kutambikia patakapokuwa peke yao, navyo vinyago vyenu vya jua vitavunjwa, nao wenzenu watakaopigwa na panga nitawatupa mbele ya magogo, mnayoyatambikia. Kweli mizoga ya wana wa Isiraeli nitaikusanya mbele ya magogo, waliyoyatambikia, nayo mifupa yenu nitaitupatupa pande zote palipo penu pa kutambikia. Pote mnapokaa miji yenu itabomoliewa, navyo vilima, mlikotambikia, vitakuwa peke yao, kusudi penu pa kutambikia pabomolewe, pawe peke yao, nayo magogo, mliyoyatambikia, yavunjwe na kukomeshwa, hata vinyago vyenu vya jua vikatwekatwe, kazi zenu zifutwe. Nao watakaouawa wataanguka katikati yenu; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Lakini wako wa kwenu, nitakaowasaza, wakipona panga, wakae kwa wamizimu katika zile nchi, mtakakotupwatupwa. Hao wenzenu watakaopona watanikumbuka huko kwa wamizimu, watakakohamishwa kwa kutekwa, kwani nitaivunja mioyo yao yenye ugoni iliyoondoka kwangu, hata macho yao nitayavunja yaliyoyatazama na kuyatamani magogo yao ya kutambikia. Ndiko, watakakojichukia machoni pao wenyewe kwa ajili ya mabaya, waliyoyafanya na kuyatumia yale matapisho yao yote. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, sikusema bure, ya kuwa nitawafanyizia hayo mabaya. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Yapige makofi yako na kupiga shindo kwa miguu yako! Kaulilie mlango wa Isiraeli kwa ajili ya matapisho mabaya yote, kwa kuwa watauawa kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya. Alioko mbali atakufa kwa ugonjwa mbaya, alioko karibu atakufa kwa upanga, aliyesalia kwa kufungiwa mjini atakufa kwa njaa. Hivyo nitawatimilizia makali yangu yenye moto. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, mizoga yao waliouawa itakapochanganyika na magogo, waliyoyatambikia po pote pa kutambikia pao: pote vilimani juu nako vileleni juu kwenye milima mikubwa yote, hata chini ya miti yote yenye majani mengi na chini ya mivule yote iliyo minene, walipoyavukizia magogo yao yote manukato ya kupendeza. Nitawakunjulia mkono wangu, nchi hii niigeuze kuwa mapori yaliyo peke yao kuanzia kwenye nyika kufikisha kwenye Dibula po pote, wanapokaa; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Wewe mwana wa mtu, hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyoiambia nchi ya Isiraeli: Mwisho uko! Huo mwisho unazijia pande zote nne za nchi hii. Sasa mwisho unakujia, nikiyatuma makali yangu, yakujie, nikupatilizie njia zako zote na kukulipisha machukizo yako yote. Jicho langu halitakuonea uchungu, wala mimi sitakuhurumia, kwani nitakulipisha njia zako, machukizo yako yatokee kwako katikati; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kibaya kimoja kitakapopita, mtaona, kibaya kingine kinakuja! Mwisho unakuja! Mwisho huo unakuja, ukuamkie! Tazama tu: unakuja! Siku yako mbaya inakuja ukaaye katika nchi hii; wakati unakuja, siku iko karibu, nayo ni ya mastuko, siyo ya kupiga vigelegele milimani. Sasa bado kidogo nitakumwagia machafuko yangu yenye moto, niyatimize kwako makali yangu, nikikupatilizia njia zako na kukulipisha machukizo yako yote. Jicho langu halitokuonea uchungu, wala mimi sitakuhurumia nikikulipisha njia zako, machukizo yako yatokee kwako katikati; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana apigaye. Itazami hiyo siku! Utaiona, inakuja! Siku mbaya imetokea! Fimbo imechanua, majivuno yamechipuka. Ukorofi umeinuka kuwa fimbo ya kuwapiga wasiomcha Mungu; hakuna chao kilichosalia, wala cha mali zao, wala cha urembo wao, wala cha utukufu wao, waliokuwa nao. Wakati umekuja, siku imetimia, ndipo asifurahi mwenye kununua, wala asisikitike mwenye kuuza, kwani makali yenye moto yanazijia mali zao zote. Kwani mwenye kuuza hatakipata tena alichokiuza, ingawa awepo na kukaa mwenye uzima, kwani hayo yaliyofumbuliwa kwa ajili ya mali zao zote hayageuki, kwa ajili ya manza, walizozikora, hakuna atakayejikalisha uzimani kwa nguvu zake. Yapigeni tu mabaragumu na kuyatengeneza yote! Hakuna atakayekwenda vitani. Kwani makali yangu yenye moto yamezijia mali zao zote. Panga ziko nje, magonjwa mabaya na njaa zimo nyumbani; alioko shambani atakufa kwa panga, naye aliomo mjini njaa na magonjwa yatamla. Nao watakaopona kwa kukimbia watakuwa milimani kama hua walioko mabondeni, hao wote watakuwa wanalia kila mtu kwa manza zake yeye, alizozikora. Mikono yote italegea, nayo magoti yote yatayeyuka kuwa kama maji. Watajifunga magunia, wakipigwa na bumbuazi sana, nyuso zao zote, zitaiva kwa kuona soni, navyo vichwa vyao vyote vitakuwa vimenyolewa. Fedha zao watazitupa barabarani, nazo dhahabu zao zitakuwa kama zenye uchafu, kwani dhahabu zao na fedha zao hazitaweza kuwaponya siku hiyo, Bwana atakapochafuka, wala hazitazishibisha roho zao, wala hazitayajaza matumbo yao, kwani ndizo zilizowaponza, wazikore manza zao. Uzuri wa hayo mapambo yao ukawatia majivuno, wakayatumia kuvitengeneza vinyago vyao vichukizavyo kwa kutapisha kwao. Kwa hiyo nimezigeuza kuwa kwao kama zenye uchafu. Kisha nitazipa mikononi mwa wageni, wazipokonye, namo mwao wasionicha katika nchi hii, waziteke, kisha wazichafue. Nami nitaugeuza uso wangu, usipatazame, wakipachafua palipokuwa urembo wangu; ndipo, wanyang'anyi watakapopaingia, wapachafue. Fanyiza minyororo! Kwani nchi hii imejaa mashauri ya damu, nao mji huu umejaa makorofi. Nami nitaleta walio wabaya kuliko wamizimu wengine, wazichukue nyumba zao; nayo majivuno yao wenye nguvu nitayakomesha, patakatifu pao pakitiwa uchafu. Mwangamizo unakuja; ndipo, watakapotafuta pa kuponea, wasipapate. Teso litafuatwa na teso jingine, zile habari mbaya zitafuatwa na habari mbaya nyingine; ndipo, watakapotafuta mfumbuaji, azifumbue, lakini watambikaji watapotelewa na Maonyo, nao wazee hawatajua mizungu. Mfalme ataomboleza, naye aliye mkuu kituko kitakuwa vazi lake, nayo mikono ya watu wa nchi hii itastushwa; nitakapowalipisha njia zao na kuwakatia shauri liyapasalo mashauri yao, ndipo watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Ikawa katika mwaka wa sita siku ya tano ya mwezi wa sita nilipokuwa nimekaa nyumbani mwangu pamoja na wazee wa Yuda waliokaa mbele yangu, ndipo, mkono wa Bwana Mungu uliponiangukia. Nilipotazama nikaona, kama ni sura ya mtu; toka hapo palipokuwa kama kiuno mpaka chini ni moto, tena toka penye kiuno mpaka juu kulionekana kuwa kama kumetuka kulikokuwa kama kwa shaba iliyong'aa sana. Kisha akakunjua kilichofanana na mkono, akanishika kishungi cha kichwani, upepo ukanichukua kuwa katikati ya nchi na ya mbingu, ukanipeleka Yerusalemu katika maono ya Kimungu pa kuliingilia lango la ndani lilioelekea kaskazini; ndipo, palipokuwa pamewekwa kinyago cha wivu kilichotia wivu. Nikauona hapo utukufu wa Mungu wa Isiraeli, kama nilivyouona katika ile mbuga ya bondeni. Akaniambia: Mwana wa mtu yaelekeze macho yako upande wa kaskazini! Nilipoyaelekeza macho yangu upande wa kaskazini, nikakiona hicho kinyago cha wivu kaskazini langoni pa kuingia penye meza ya kutambikia. Akaniambia: Mwana wa mtu, unayaona, hao wanayoyafanya? Ni machukizo makubwa, watu wa mlango wa Isiraeli wanayoyafanya hapa, niondoke Patakatifu pangu mwenda mbali. Tena utaona mengine yaliyo machukizo makubwa zaidi. Kisha akanipeleka langoni penye ua; nilipotazama nikaona tundu moja ukutani. Akaniambia: Mwana wa mtu, penya humu ukutani! Nikapenya mle ukutani, nikaona mlango mmoja. Akaniambia: Ingia, uyaone hayo machukizo mabaya, hao wanayoyafanya hapo! Basi, nikaingia; nilipotazama nikaona kila mfano wa wadudu na wa nyama watapishao, nayo magogo yote, wao wa mlango wa Isiraeli wanayoyatambikia, yalikuwa yamechorwa ukutani kupazunguka po pote. Mbele yao walikuwa wamesimama wazee 70 wa mlango wa Isiraeli, naye Yazania, mwana wa Safani, alisimama katikati yao; kila mtu alishika chetezo mkononi mwake, mvuke wa moshi wa uvumba ukapanda juu. Akaniambia: Umeyaona, mwana wa mtu, wazee wa mlango wa Isiraeli wanayoyafanya gizani kila mmoja katika vyumba vyake vya vinyago? Kwani husema: Hakuna Bwana anayetuona, Bwana ameondoka katika nchi hii. Akaniambia: Utaona tena mengine yaliyo machukizo makubwa zaidi, hao wanayoyafanya. Akanipeleka penye lango la kuingia Nyumbani mwa Bwana lililoko upande wa kaskazini, nikaona humo wanawake waliokaa wakimlilia Tamuzi. Akaniambia: Umeyaona, mwana wa mtu? Utaona tena mengine yaliyo machukizo mabaya kuliko haya. Akanipeleka katika ua wa ndani wa Nyumba ya Bwana, nikaona hapo pa kuliingilia Jumba la Bwana katikati ya ukumbi na meza ya kutambikia waume kama 25, walikuwa wameligeuzia Jumba la Bwana migongo yao, lakini nyuso zilielekea upande wa maawioni kwa jua, wakiliangukia jua na kuyaelekea maawio yake. Akaniambia: Umeyaona, mwana wa mtu? Je? Kuyafanya haya machukizo, wanayoyafanya hapa, hakukuutoshea mlango wa Isiraeli? Imekuwaje, wakiieneza nchi makorofi ya kunikasirisha mara kwa mara? Watazame, jinsi wanavyoyashika yale machipuko ya miti mbele ya pua zao. Mimi nami nitawatolea makali yangu yenye moto; jicho langu halitawaonea uchungu, wala mimi sitawahurumia; ingawa wanililie masikioni kwa sauti kuu, sitawasikia kabisa. Akaita kwa sauti kuu masikioni mwangu kwamba: Mapatilizo ya mji huu yamekaribia; kila mtu na ashike mkononi mwake chombo chake cha kuangamizia! Nikaona watu sita, waliotokea katika njia ya lango la juu lililoelekea kaskazini, kila mtu alikuwa ameshika mkononi mwake chombo chake cha kupondea; lakini mtu mmoja aliyekuwa katikati yao alikuwa amevaa vazi la ukonge, napo kiunoni pake alikuwa na kichupa cha wino cha mwandishi, wakaja, wakasimama kando ya meza ya shaba ya kutambikia. Ndipo, utukufu wa Mungu wa Isiraeli ulipoondoka kwenye Kerubi, ulikokuwa, ukaja kwenye kizingiti cha mlango wa hiyo nyumba, akamgutia yule mtu aliyevaa vazi la ukonge, aliyekuwa na kichupa cha wino cha mwandishi kiunoni pake. Bwana akamwambia: Pitia humu mjini katikati, humu Yerusalemu katikati, uwaandike kichoro mapajini wale watu wapigao kite na kuyaugulia hayo machukizo yote yafanyikayo humu mjini! Wale wengine akawaambia masikioni pangu: Piteni humu mjini nyuma yake, kapigeni! Macho yenu yasiwaonee uchungu, wala msiwahurumie! Wazee, wasichana, wavulana, watoto, wanawake, waueni wote pia, waangamie! Lakini kila mtu mwenye kichoro msimguse kabisa! Anzieni hapa Patakatiu pangu! Wakawanzia wale wazee waliokuwa mbele ya hiyo Nyumba. Kisha akawwambia: itieni Nyumba hii uchafu, nkizijaza nyua zake mizoga yao waliouawa! Kisha tokeni! Basi, wakatoka humo, wakawapiga mjini namo. Ikawa walipokwenda kuwapiga watu vivyo, hivyo, mimi nikasalia hapo peke yangu; ndipo, nilipoanguka kifudifudi, nikalia nikisema: E Bwana Mungu, wewe utayaangamiza masao yote ya Isiraeli, ukiumwagia Yerusalemu makali yako yenye moto? Akaniambia: Manza za mlango wa Isiraeli na wa Yuda ni kubwa sanasana, nchi hii imeenezwa damu, walizozimwaga, mji huu nao ikajaa mapotovu, kwani husema: Bwana ameondoka katika nchi hii, hakuna Bwana anayeyaona. Basi, mimi nami jicho langu halitawaonea uchungu, wala mimi sitawahurumia, nitawapatilizia njia zao vichwani pao. Kisha nikamwona yule mtu aliyevaa nguo ya ukonge aliyekuwa na kichupa cha wino kiunoni pake, akileta majibu kwamba: Nimefanya, kama ulivyoniagiza. Nilipotazama penye ukingo uliokuwa juu ya vichwa vyao Makerubi nikaona kilichokuwa kama kito cha Safiro, kikafanana sura yake kuwa kama kiti cha kifalme, kikaonekana kuwa juu yao. Akamwambia yule mtu aliyevaa vazi la ukonge, akasema: Ingia katikati ya magurudumu yaliyo chini ya Makerubi, uvijaze viganja vyako makaa ya moto yaliyoko katikati ya Makerubi, kisha yamwagie mji huu! Ndipo, alipopaingia machoni pangu. Makerubi yalikuwa yamesimama kuumeni penye hiyo Nyumba, yule mtu alipoingia, nalo lile wingu lilikuwa limeujaza ua wa ndani. Utukufu wa Bwana ukaondoka kwa Makerubi kwenda penye kizingiti cha kuiingilia hiyo Nyumba, hiyo Nyumba ikajazwa na lile wingu, ua nao ukajaa ung'avu wa utukufu wa Bwana. Uvumi wa mabawa ya Makerubi ukasikilika mpaka kwenye ua wa nje, ukawa kama sauti ya Mwenyezi Mungu, akisema. Ikawa, alipomwagiza yule mtu aliyevaa vazi la ukonge kwamba: Chukua moto penye magurudumu katikati ya Makerubi, naye alipoingia na kusimama kando ya gurudumu, ndipo, Kerubi alipokunjua mkono wake kwenye Makerubi na kuupeleka penye moto uliokuwa katikati ya Makerubi, akautwaa, akampa mwenye vazi la ukonge na kuutia katika viganja vyake, naye akauchukua, akatoka. Kisha kukaoneka kwa Makerubi chini ya mabawa yao mfano wa mkono wa mtu. Nilipotazama mara nikaona magurudumu manne kando ya Makerubi, gurudumu moja kando ya Kerubi mmoja, vivyo hivyo gurudumu moja kando ya kila Kerubi mmoja; nilipoyatazama hayo nagurudumu, jinsi yalivyokuwa, yalikuwa kama kito cha Tarsisi. Yote manne mfano wao ulionekana kuwa mmoja, ulikuwa kama gurudumu moja lililomo ndani ya gurudumu lenziwe. Yalipokwenda yalikwenda pande zote nne pasipo kugeuka katika mwendo wao, kwani mahali hapo, kichwa kilipoelekea, ndipo, walipopafuata pasipo kugeuka katika mwendo wao. Nayo miili yao na migongo yao na mikono yao na mabawa yao, nayo magurudumu yalikuwa yamejaa macho po pote, penye magurudumu yote manne vilikuwa hivyo. Hayo magurudumu yakaitwa masikioni pangu Kimbunga. Kila Kerubi mmoja alikuwa na nyuso nne: Uso mmoja ulikuwa wa Kerubi, uso wa pili ulikuwa wa mtu, wa tatu ulikuwa wa simba, wa nne ulikuwa wa tai. Kisha Makerubi wakaenda juu. Hawa ndio nyama, niliyemwona kwenye mto wa Kebari. Makerubi walipokwenda, magurudumu yakaenda kando yao; tena Makerubi walipoyakunjua mabawa yao, waondoke katika nchi kwenda juu, magurudumu nayo hayakugeuka kuondoka kando yao. Waliposimama, nayo yakasimama; walipoinuka kwenda juu, nayo yakajiinua kwenda juu pamoja nao, kwani roho ya huyo nyama ilikuwa namo katika hayo magurudumu. Kisha utukufu wa Bwana ukatoka kwenye kizingiti cha kuiingilia hiyo Nyumba, ukasimama juu ya Makerubi. Makerubi wakayakunjua mabawa yao, wakaondoka katika nchi kwenda juu machoni pangu; ndivyo, walivyotoka hapo, hayo magurudumu hayo yakawa kandokando yao; wakasimama tena kwenye lango la Nyumba ya Bwana lielekealo maawioni kwa jua, nao utukufu wa Mungu wa Isiraeli ulikuwa juu yao. Huyo ndiye nyama, niliyemwona chini yake Mungu wa Isiraeli kwenye mto wa Kebari, nikajua, ya kuwa hao ndio Makerubi. Kila mmoja wao alikuwa na nyuso nne, tena kila mmoja alikuwa na mabawa manne, tena iliyofanana na mikono ya watu ilikuwa chini ya mabawa yao. Nazo nyuso zao hao zilikuwa zimefanana na zile nyuso, nilizoziona kwenye mto wa Kebari; ndivyo, zilivyoonekana kuwa, nao wenyewe walikuwa hivyo. Kila mmoja wakaenda na kufuata hapo, uso wake ulipoelekea. Roho ikanichukua, ikanipeleka kwenye lango la Nyumba ya Bwana la mashariki lielekealo maawioni kwa jua. Hapo pa kulilingilia lile lango nikapaona waume 25; katikati yao nikamwona Yazania, mwana wa Azuri, na Pelatia, mwana wa Benaya, walio wakuu wa ukoo huu. Akaniambia: Mwana wa mtu, hawa waume ndio wanaowaza yaliyomaovu na kuwapigia watu mashauri mabaya humu mjini. Ndio wanaosema: Kujenga nyumba siko karibu; mji huu ndio nyungu, nasi ndio nyama. Kwa hiyo wafumbulie yatakayokuwa! Wafumbulie, mwana wa mtu! Ndipo, Roho ya Bwana iliponiangukia, ikaniambia: Sema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ndivyo, mlivyosema, mlio wa mlango wa Isiraeli, nayo mawazo yainukayo rohoni mwenu mimi nimeyajua. Wenzenu, mliowaua humu mjini, ni wengi, mkajaza barabara za mji mizoga yao. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wenzenu, mliowaua na kuwalaza humu mjini, hao ndio nyama, nao mji huu ndio nyungu, lakini ninyi watawatoa humu mjini. Panga mnaziogopa, lakini nitawaletea panga; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Kisha nitawatoa humu mjini, niwatie mikononi mwa wageni; ndipo, nitakapowakatia mashauri. Mtauawa kwa panga, kwenye mipaka ya Isiraeli ndiko, nitakakowapatiliza; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Mji huu hautakuwa nyungu yenu, mkiwa nyama humu mjini, ila kwenye mipaka ya Isiraeli ndiko, nitakakowapatiliza. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana; hamkuyafuata maongozi yangu, wala hamkuyafanya mashauri yangu, ila mmefanya, kama wamizimu wawazungukao wanavyopiga mashauri. Ikawa, nilipowafumbulia haya, ndipo, Pelatia, mwana wa Benaya, alipokufa; nikaanguka kifudifudi na kulia kwa sauti kuu nikisema: E Bwana Mungu, wewe utalimaliza sao lake Isiraeli! Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, ndugu zako, hawa ndugu zako, ambao mlitekwa pamoja nao, hata mlango wote wa Isiraeli, hawa wote ndio, wenyeji wa Yerusalemu waliowaambia: Nendeni mbali mkitoka kwake Bwana! Sisi tumepewa nchi hii, iwe yetu! Kwa hiyo sema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema kwamba: Kweli nimewapeleka mbali kwenye wamizimu na kuwatawanya katika hizo nchi siku hizi zilizo chache, nikawa mwenyewe patakatifu pao katika nchi hizo, walikopelewa. Kwa hiyo sema: Hivi ndivyo Bwana Mungu anavyosema: Nitawakusanya ninyi na kuwatoa katika hayo makabila, kweli nitawaunganisha ninyi na kuwatoa katika nchi hizo, nilikowatawanya, niwape ninyi nchi ya Isiraeli. Napo watakapoiingia watayaondoa huko matapisho yake yote na machukizo yake yote. Nami nitawapa kuwa moyo mmoja, tena nitatia roho moja mioyoni mwao; namo miilini mwao nitaitoa mioyo iliyo migumu kama mawe nikiwatia mioyo inayolegea kama nyama. Ndivyo, watakavyoyafuata maongozi yangu na kuyashika mashauri yangu, wayafanye. Watakuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Lakini wenye mioyo iyaelekeayo matapisho yao na machukizo yao, mioyo yao ikayafuata, basi, nitawapatilizia njia zao vichwani pao. Ndipo, Makerubi walipoyakunjua mabawa yao, nayo magurudumu yakawa kando yao, nao utukufu wa Mungu wa Isiraeli ukawa juu yao. Kisha utukufu wa Bwana ukapanda ukiondoka mle mjini katikati, ukasimama juu ya mlima ulioko karibu ya mji upande wa maawioni kwa jua. Roho ikanichukua, ikanipeleka katika nchi ya Wakasidi kwenye mateka kwa nguvu ya hayo maono ya Roho ya Mungu. Kisha hayo maono, niliyoyaona, yakaniondokea. Nikawaambia waliotekwa mambo yote ya Bwana, aliyonionyesha. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu unakaa katikati ya mlango mkatavu, wako na macho yaonayo, lakini hawaoni, wako na masikio yasikiayo, lakini hawasikii, kwani hawa ndio mlango mkatavu. Basi, wewe mwana wa mtu, jifanyizie vyombo vya kuhama navyo! Kisha hama mchana machoni pao, ukuhama mahali pako na kuhamia pengine machoni pao, labda wataona, ya kuwa ndio mlango mkatavu. Navyo vyombo vyako utavitoa nyumbani mchana machoni pao, kama ni vyombo vya kuhama navyo, nawe utatoka nyumbani jioni machoni pao, kama watu wanavyotoka mwao wakitaka kuhama. Machoni pao bomoa bomani kwa mji, pawe tundu, ndipo uvitolee vyombo vyako! Machoni pao uviweke begani, uvitoe, giza ikiwa kuu! Nao uso wako uufunike, usiione nchi! Kwani nimekuweka kuwa kielekezo cha mlango wa Isiraeli. Nikafanya hivyo, nilivyoagizwa: vyombo vyangu nikavitoa mchana, kama ni vyombo vya kuhama navyo, kisha nikajibomolea kwa mikono tundu bomani kwa mji, nikavitoa, giza ilipokuwa kuu, nikiviweka begani machoni pao. Asubuhi neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, wao wa mlango wa Isiraeli walio mlango mkatavu hawakukuuliza: Wewe unafanya nini? Waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Tamko hili zito ni la mkuu wa Yerusalemu, tena la mlango wote wa Isiraeli uliomo humu mjini. Sema: Mimi ni kielekezo chenu; kama mimi nilivyofanya, ndivyo, nao watakavyofanyiziwa, watahamishwa kwenda kifungoni. Naye mkuu aliomo mwao mjini atavichukua vyombo vyake begani, giza ikiwa kuu, akitoka katika tundu la bomani kwa mji, walilombomolea, wapate kumtoa hapohapo; uso wake utaufunika, kusudi asiione nchi kwa macho yake. Nami nitamtegea wavu wangu, anaswe katika tanzi langu; kisha nitampeleka Babeli katika nchi ya Wakasidi, lakini hataiona; nako ndiko, atakakokufa. Nao wote wamzungukao kuwa wasaidiaji wake nao wa vikosi vyake vyote nitawatupatupa pande zote za upepo, nazo panga nitazichomoa, ziwafuate nyuma. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapowatupatupa kwenye wamizimu na kuwatawanya katika nchi hizo. Lakini nitasaza kwao wachache wanaohesabika, wasiuawe na panga, wala na njaa, wala na magonjwa mabaya, wapate kuyasimulia machukizo yao yote kwenye wamizimu, watakakopelekwa, nao wajue, ya kuwa mimi ni Bwana. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, sharti ukile chakula chako kwa kutetemeka! Nayo maji yako sharti uyanywe kwa kustuka na kwa kuyahangaikia. Kisha waambie watu wa nchi hii: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyowaambia wakaao Yerusalemu katika nchi ya Isiraeli: Vyakula vyenu mtavila na kuvihangaikia, nayo maji yenu mtayanywa kwa kupigwa na bumbuazi, kwani nchi yao itaangamia, yote yaliyojaa mle yakipotea kwa ajili ya ukorofi wao wote waliokaa huko. Nayo miji inayokaa watu itabomolewa, nchi hii iwe peke yake tu; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, ni fumbo gani hili lililoko kwenu katika nchi ya Isiraeli la kusema: Siku hukawia, nayo maono yote hupotea? Kwa hiyo waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nitalikomesha fumbo hilo, wasilitumie tena kwao Waisiraeli; kwa hiyo waambie: Siku hizo ziko karibu kweli, maono yote yatimie. Kwani hakuna tena ono lo lote litakalokuwa la bure, wala ufumbuaji wa kupendeza watu tu kwao wa mlango wa Isiraeli. Kwani mimi Bwana nitasema, nayo nitakayoyasema yatafanyizwa pasipo kukawia kabisa, kwani katika hizi siku zenu, mngalipo bado, ninyi mlio mlango mkatavu, nitasema neno, kisha nitalifanya! Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, tazama, wao wa mlango wa Isiraeli husema: Ono, analoliona yeye, ni la siku nyingi, nayo maneno, anayoyasema yeye, wakati wao wa kutimia uko mbali. Kwa hiyo waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Maneno yangu yote yahatakawia tena; neno, nitakalolisema, litafanyizwa; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu wafumbuaji wa Isiraeli wanaowafumbulia yatakayokuwa wafumbulie wewe yatakayowajia. Waambie hao wafumbuaji wanaosema kwa hayo yaliyomo mioyoni mwao: Lisikieni neno la Bwana! Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wafumbuaji hawa wajinga watapatwa na mambo! Maana huzifuata roho zao, husema mambo, wasiyoyaona! Kama mbweha walivyo kwenye mabomoko, ndivyo, wafumbuaji wako, Isiraeli, walivyo. Hamkukwea hapo palipoatuka nyufa, wala hamkuuzungushia mlango wa Isiraeli boma, wapate kusimama kwenye mapigano, siku ya Bwana itakapokutia. Wameona maono yasiyokuwako, nayo maaguo yao ni ya uwongo, wakisema: Ndivyo, asemavyo Bwana, lakini Bwana hakuwatuma, nao wakangojea, alitimize neno lao. Je? Hamkuona maono yasiyokuwako? Hamkusema maaguo ya uwongo, mliposema: Ndivyo, asemavyo Bwana, nami nalikuwa sikuyasema? Kwa hiyo Bwana Mungu anasema: Kwa kuwa mmesema yasiyokuwako, mkaona mambo ya uwongo, kwa hiyo mtaniona, nikiwajia ninyi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Itakuwa, mkono wangu uwajie hao wafumbuaji walioona yasiyokuwako na kuagua uwongo; hawatakula bia nao walio ukoo wangu, wala hawataandikwa katika kitabu cha mlango wa Isiraeli, wala hawataiingia nchi ya Isiraeli; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu. Wanawapoteza mara kwa mara walio ukoo wangu wakisema: kumetengemana, lakini utengemano hauko; tena watu wakijenga boma wenyewe, hao utawaona, wakilipaka chokaa. Kwa sababu hii waambie hao mafundi wa kupaka chokaa: Litaanguka! Itakunya mvua ifurikayo maji, nami nitanyesha mvua ya mawe, yaliangukie, hata upepo wa kimbunga utalibomoa; ndipo, mtakapoona, hilo boma likianguka, nanyi mtaulizwa: Chokaa, mliyolipaka, iko wapi? Kweli hivyo ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwani machafuko yangu yenye moto nitaleta upepo wa kimbunga wa kulibomoa, hata mvua ifurikayo maji itakunya kwa makali yangu, nayo mvua ya mawe ya kuangamiza itaanguka kwa yale machafuko yangu yenye moto. Ndipo, nitakapolibomoa boma, mlilolipaka chokaa, nitaliangusha chini, msingi wake utokee; napo, litakapoanguka, mtaangamia huko katikati. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Hayo machafuko yangu yenye moto nitayamaliza huko katika hilo boma nako kwao waliolipaka chokaa, kisha nitawaambia: Hilo boma haliko tena, wala hao waliolipaka chokaa hawako tena. Nao ndio waliokuwa wafumbuaji wa Isiraeli walioufumbulia Yerusalemu yatakayokuwa na kuupatia maono yenye utengemano, utengemano usipokuwa kabisa; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Wewe mwana wa mtu, uso wako uuelekezee wanawake wa ukoo wako wanaoagua kwa hayo yaliyomo mioyoni mwao, uwafumbulie yatakayowajia! Sema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Watapatwa na mambo hao wanawake wanaoshona vitambaa vya uganga katika maungo yote ya mikono, wanaotengeneza hata miharuma ilinganayo na vichwa vya kila umbo, kusudi wapate kunasa roho za watu! Je? Mwataka kuzinasa roho zao walio ukoo wangu, mziokoe roho zenu wenyewe? Mkanitia uchafu mbele yao walio wa ukoo wangu mkiweza kupata makufi mawili tu ya mawele au vipande vichache vya mkate; ndivyo, mnavyoziua roho za watu wasioipaswa na kufa, nazo roho za wengine wasiopaswa na kupona mnaziponya, mkiwaogopea walio ukoo wangu, wanaopenda kusikia maneno ya uwongo. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikivijia vitambaa vyenu vya uganga, mnavyovitumia vya kunasia roho za watu, kama ni ndege, nitavirarua mikononi mwenu, nizinasue zile roho za watu kwenda zao, ni zile roho, mlizozinasa, kama ni ndege. Nayo miharuma yenu nitairarua, niwaokoe mikononi mwenu walio ukoo wangu, wasiwe mateka tena mikononi mwenu. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Kwa madanganyo yenu mmeiumiza mioyo yao waongofu, nisiowaumiza mimi, mkaishupaza mikono yao wasionicha, wasiweze kurudi katika njia zao mbaya, wapate uzima. Kwa sababu hii hamtaona tena maono yasiyokuwako, wala hamtaagua tena maaguo, kwani walio ukoo wangu nitawaponya mikononi mwenu; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Wakaja kwangu waume wazee wa Kiisiraeli, wakakaa mbele yangu. Ndipo, neno la Bwana liliponijia la kwamba: Mwana wa mtu, watu hawa wameyatia magogo yao ya kutambikia mioyoni mwao, wakayaweka mbele ya nyuso zao kuwa kwazo la kuwakosesha; sasa je? Niwaitikie nikitafutwa nao? Kwa hiyo sema nao na kuwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtu ye yote wa mlango wa Isiraeli atakayeyatia magogo yake ya kutambikia moyoni mwake na kuyaweka mbele ya uso wake kuwa kwazo la kumkosesha, kisha akija kwa mfumbuaji, basi, mimi Bwana nitamjibu yayapasayo magogo yake mengi ya kutambikia, kusudi niipate mioyo yao walio mlango wa Isiraeli waliotawanyika wote na kuniacha kwa ajili ya magogo yao ya kutambikia. Kwa hiyo waambie walio mlango wa Isiraeli: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Rudini! Jigeuzeni na kuyaacha magogo yenu ya kutambikia! Zigeuzeni nyuso zenu na kuyaacha machukizo yenu yote! Kwani mtu ye yote wa mlango wa Isiraeli, nao walio wageni wakikaa kwa Waisiraeli, wote pia wametawanyika wakiacha kunifuata; hao wakiyatia magogo yao ya kutambikia mioyoni mwao na kuyaweka mbele ya nyuso zao kuwa kwazo la kuwakosesha, kisha wakija kwa mfumbuaji, aniulize kwa ajili yao, basi, mimi Bwana nitawajibu mwenyewe. Mtu aliye hivyo nitamkazia macho yangu, nitamwangamiza vibaya, awe kielekezo na fumbofumbo, nikimtowesha kwao walio ukoo wangu; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Kama yuko mfumbuaji aliyeshindwa naye, akamwambia mtu aliye hivyo neno lo lote, mimi Bwana nimemshinda huyo mfumbuaji, tena nitamkunjulia mkono wangu, nimtoweshe kwao walio ukoo wangu wa Isiraeli. Hivyo watatwikwa manza zao walizozikora: manza zake aliyeuliza zitakuwa sawasawa na manza zake mfumbuaji yule. Kusudi walio mlango wangu wa Isiraeli wasipotee tena wakiacha kunifuata na kujipatia uchafu tena kwa mapotovu yao yote, wapate kuwa ukoo wangu, nami nipate kuwa Mungu wao; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, nchi ikinikosea na kuvunja maagano, nitaikunjulia mkono wangu, nilivunje shikizo lao la chakula na kuipelekea njaa, nimalize huko watu na nyama. Lakini kama wangekuwako katika ile nchi watu hawa watatu: Noa na Danieli na Iyobu, hawa wangejiponya kwa wongofu wao; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Kama ningeleta nyama wabaya, watembee katika ile nchi na kuwamaliza watu walioko, iwe peke yake, asipite mtu kwa ajili ya wale nyama, basi, kama wangekuwako katika ile nchi hao watu watatu: hivyo, nilivyo Mwenye uzima, ndivyo, Bwana Mungu asemavyo, nao hawataponya wana wa kiume wala wa kike, ila wangepona wao wenyewe tu, hiyo nchi iwe peke yake. Au kama ningeiletea ile nchi panga nikisema: Panga na zitembee katika nchi hii, nitoweshe kwake watu na nyama, kama wangekuwako katika ile nchi hao watu watatu: hivyo, nilivyo Mwenye uzima, ndivyo, Bwana Mungu asemavyo, hawataponya wana wa kiume waka wa kike, ila wangepona wao wenyewe tu. Au kama ningeipelekea ile nchi magonjwa mabaya, akiimwagia makali yangu yenye moto pamoja na kumwaga damu, nitoweshe kwake watu na nyama, kama wangekuwako katika ile nchi Noa na Danieli na Iyobu: hivyo, nilivyo Mwenye uzima, ndivyo, asemavyo Bwna Mungu, hawataponya mwana wa kiume wala wa kike, ila wengepona wao wenyewe tu kwa wongofu wao. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Ingawa niupelekee Yerusalemu haya mapatilizo yangu manne yaliyo mabaya: panga na njaa na nyama wabaya na magonjwa mabaya, nitoweshe mwake watu na nyama, mtaona, wakisazwa mwake waliopona watakaohamishwa wa kiume na wa kike, hao mtawaona wakitokea kwenu, mzitazama njia zao na matendo yao; ndipo, mtakapoituliza mioyo yenu kwa ajili ya mabaya, niliyouletea Yerusalemu, na kwa ajili yao yote, niliyouletea. Wataituliza mioyo yenu, mtakapozitazama njia zao na matendo yao; ndipo, mtakapojua, ya kuwa sikuyafanya bure tu hayo yote, niliyoufanyia; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, mti wa mzabibu unaipita miti yote kwa nini? Au liko, tawi lake linalolipata likikaa kwenye miti ya mwituni? Je? Huchukuliwa mti wake wa kutumiwa kwa kazi yo yote? Au watu huuchukua, wautumie kuwa mambo tu ya kutungikia vyombo vyao? Mtauona, nikiutoa kuwa kuni za moto; moto ukiisha kuzila pande zake mbili za mwisho, nacho kipande cha katikati kikiungua, Je? Iko kazi, utakayotumikia? Tazameni! Ungaliko mzima bado hautumiwi kwa kazi yo yote; sembuse moto ukiisha kuula na kuunguza, hautatumiwa kabisa kwa kazi yo yote. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kama mti wa mzabibu ulioko kwenye miti ya mwituni nilivyoutoa kuwa kuni za moto tu, ndivyo, nitakavyowatoa wakaao Yerusalemu. Nitawakazia macho yangu: ijapo wametoka motoni, moto ndio utakaowala; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapowakazia macho yangu. Nayo nchi hii nitaigeuza kuwa peke yake tu, kwa kuwa wamevunja maagano; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, wajulishe Wayerusalemu machukizo yao ukiwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyouambia Yerusalemu: Nchi ya Kanaani ndiko kwenu kwa mwanzo wako na kwa kuzaliwa kwako; baba yako ni Mwamori, mama yako ni Mhiti. Nako kuzaliwa kwako kulikuwa hivyo: siku ulipozaliwa hukukatwa kitovu, wala hukuogoshwa maji, utakate, wala hukupakwa chumvi hata kidogo, wala hukuvikwa nguo za kitoto. Halikuwako jicho lililokuonea uchungu wa hukufanyizia moja tu la mambo hayo kwa lililokuonea uchungu wa kukufanyizia moja tu la mambo hayo kwa kukuhurumia, ila ulitupwa shambani, kwa kuwa waliichukia roho yako siku, ulipozaliwa. Nikapita hapo, ulipokuwa, nikakuona ulivyogaagaa katika damu yako nikakuambia: Hivyo, unavyolala katika damu yako, uwe mzima! Nikakuambia kweli: Hivyo unavyolala katika damu yako, uwe mzima! Nitakupa kuwa maelfu na maelfu, kama majani ya shambani yalivyo mengi. Ndipo, ulipokua na kuendelea hivyo, mpaka ukawa mkubwa, ukapata kuwa mzuri zaidi, maziwa yako yakapata nguvu nazo nywele zako zikaota sana, lakini wewe ulikuwa ungaliko uchi bado pasipo kufunikwa na nguo. Nikapita hapo, ulipokuwa, nikakuona, ya kuwa siku zako za kuvunja ungo zimetimia, nikakutandia guo langu la kujifunika, nikaufunika uchi wako, nikakuapia na kukufanya agano na wewe, nawe ukawa wangu; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Kisha nikakuogesha maji na kukumwagia mengi, damu yako ikutoke kabisa, nikakupaka mafuta. Nikakuvika nguo za rangi, nikakupa hata viatu vya ngozi ya pomboo, nikakufunga nao mharuma wa bafta, nikakupa ukaya wa hariri. Kisha nikakupamba kwa mapambo: nikakupa vikuku vya kuvaa mikononi pako na mkufu wa shingoni pako. Nikakupa navyo vipini vya puani na mapete ya masikioni na kilemba chenye utukufu kichwani pako. Hivyo ulipata mapambo ya dhahabu na ya fedha na mavazi ya bafta na ya hariri na ya nguo za rangi, ukala vikate vya unga uliopepetwa vema sana na asali na mafuta, ukawa mzuri sanasana, ukafanikiwa kupata macheo ya kifalme. Uvumi wako ukatoka, ukaenea kwa mataifa, kuwa uzuri wako ndio uzuri uliotimilika kabisa kwa ajili ya urembo, niliokutia; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Lakini ukajiegemezea uzuri wako, ukafanya ugoni, kila aliyepita ukamtupiatupia mapendeleo yako, ukawa wake. Ukachukua mavazi yako, ukajitengenezea pa kutambikia milimani, ukapapamba nguo za rangi; ndiko, ulikofanyizia ugoni usiokuwa kale, wala hautakuwa tena. Kisha ukayachukua mapambo yako matukufu yaliyo dhahabu zangu na fedha zangu, nilizokupa, ukajitengenezea vinyago vya kiume, ukafanya ugoni navyo. Ukayachukua nayo mavazi yako ya nguo za rangi, ukavivika, ukavipelekea nayo mafuta yangu na uvumba wangu kuwa mbele yao. Hata vikate vyangu, nilivyokupa vya unga uliopepetwa vema sana, na mafuta na asali, niliyokulisha, ukayatoa mbele yao kuwa uvukizo wenye mnuko wa kupendeza. Ndivyo, ilivyokuwa kweli; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Ukawachukua nao wanao wa kiume na wa kike, uliowazaa, wawe wangu, ukawatoa kuwa ng'ombe zao za tambiko na chakula chao. Je? Ugoni wako haukutosha, ukiwachinja wanangu, ukawatoa na kuwapitisha motoni, wawe wao? Ulipoyafanya machukizo yako yote na ugoni wako wote hukuzikumbuka siku za utoto wako za kuwa uchi pasipo kufunikwa na nguo, ulipokuwa unagaagaa katika damu yako? Kwa kuwa umekwisha kuyafanya hayo mabaya yako yote, yatakupata! Yatakupata kweli! ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Kisha ukajijengea nyumba ya vinyago, uwanjani po pote ukajitengenezea pa kutambikia. Pembeni po pote penye barabara ukajenga pako pa kutambikia, nao uzuri wako ukautumia, mpaka ukiwa chukizo, ukimpanulia kila aliyepita miguu yako, ukauzidisha ugoni wako. Ukafanya ugoni nao Wamisri, uliokaa nao, walio wenye miili mikubwa, ukauzidisha ugoni, kusudi unikasirishe. Mara nikakukunjulia mkono wangu, nikakupunguzia yakupasayo, nikakutia mikononi mwao wakuchukiao, wakufanyie wayatakayo, ni wale wanawake wa Kifilisti waliopatwa na soni kwa ajili ya njia zako zenye uzinzi. Ukafanya ugoni nao wana wa Asuri, kwa kuwa hujashiba bao; ukafanya ugoni nao, lakini hapo napo hukushiba. Ukauzidisha ugoni wako katika nchi ya Kanaani mpaka huko, Wakasidi wanakokaa, lakini hapo napo hukushiba. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Kweli moyo wako ulikuwa unatamani sana kupendwa, ukiyafanya hayo yote yanayofanywa na mwanamke mgoni asiyejua soni. Ilikuwa hapo, ulipovojenga vyumba vyako vya vinyago po pote barabarani pembeni, ulipopatengeneza pako pa kutambikia uwanjani po pote. Tena hukuwa kama mwanamke mgoni aubeuaye mshahara. U mwanamke avunjaye unyumba, achukuaye wageni na kumwacha mumewe. Watu huwapa wanawake wagoni mapenyezo, lakini wewe huwapa wote wanaokupenda matunzo yako; ukiwagawia hayo, unataka, wakujie na kutoka po pote, wafanye ugoni na wewe. Kwako, ukifanya ugoni, mambo yamegeuka, yasiwe kama kwa wanawake wengine: wewe hutakiwi ugoni wakikufuatafuata, ila huwapa mshahara wewe, usipewe mwenyewe mshahara; hivyo ndivyo, vilivyogeuka. Kwa hiyo, wewe mwanamke mgoni, lisikie neno la Bwana: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa mapesa yako yamemwagwa, tena kwa kuwa unapofanya ugoni nao wote wakupendao hujifunulia nguo machoni pao, wauone uchi wako, hata kwenye magogo ya kutambikia yachukizayo, tena kwa kuwa umezimwaga damu za wanao, unaowapa, wawe wao: kwa hiyo utaniona, nikiwakusanya wote waliokupenda, ndio uliowapendeza, nao wote uliowapenda, nao wote uliowachukia, hao wote nitawakusanya, wakujie na kutoka po pote, kisha nitaufunua uchi wako wote. Kisha nitakupatiliza mapatilizo ya wanawake wavunjao unyumba nayo yao waliomwaga damu; hivyo nitakutoa, damu yako imwagwe kwa makali yenye moto na kwa wivu. Tena nitakutia mikononi mwao, wavivunje vyumba vyako vya vinyago, wapabomoe pako pa kutambikia, wakuvue nayo mavazi yako na kuyachukua mapambo yako matukufu, kisha wakuache, ukiwa mwenye uchi pasipo kujifunika kwa nguo. Kisha watakukusanyikia mkutano mkubwa, watakupiga mawe, kisha watakukatakata kwa panga zao. Nazo nyumba zako wataziteketeza kwa moto, wakutimilizie mapatilizo machoni pa wanawake wengi. Hivyo ndivyo, nitakavyokukomesha, usifanye ugoni tena, wala usilipe mshahara wa ugoni. Hivyo nitayatimiza kwako makali yangu yenye moto, wivu wangu uondoke kwako, nipate kutulia, nisikasirike tena. Kwa kuwa hukuzikumbuka siku za utoto wako, ukanichafua roho kwa kuyafanya hayo yote, kwa ajili ya hayo yote utaniona nami, nikikutwika njia yako kichwani; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Je? Hukuyaongeza machukizo yako yote kwa kufanya uzinzi? Itakuwa kila atumiaye mafumbo atakuambia fumbo hilo la kwamba: Kama mama alivyo, ndivyo, mwanawe wa kike alivyo. Wewe ndiwe mwana wa mama yako aliyemkumba mumewe pamoja na watoto wake, tena ndiwe dada ya ndugu zako wa kike waliowakumba waume zao pamoja na watoto wao; mama yenu ni Mhiti, naye baba yenu ni Mwamori. Dada yako mkubwa akaaye kushotoni kwako ni Samaria, yeye mwenyewe na wanawe; naye dada yako mdogo akaaye kuumeni kwako ni Sodomu na wanawe. Wewe kwanza hukuzifuata njia zao, wala hukufanya machukizo kama yao. Lakini ilikuwa punje kidogo tu, kisha ukafanya mabaya yaliyo makuu kuliko yao katika njia zako zote. Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, ndivyo, asemavyo Bwana Mungu, dada yako mdogo Sodomu na wanawe hawakufanya mabaya, kama wewe na wanao mlivyofanya. Tazama, hayo, dada yako mdogo Sodomu na wanawe waliyoyafanya, yalikuwa maovu: majivuno na shibe za vyakula na utulivu wa kutengemana tu; hayo alikuwa nayo yeye mwenyewe na wanawe, lakini hawakuishikiza mikono ya wanyonge wala ya wakiwa. Wakajikuza, wakafanya yaliyo machukizo machoni pangu, nikawaondoa, nilipoyaona. Naye Samaria makosa yake hayafiki kuwa nusu ya makosa yako wewe, ukayazidisha machukizo yako kuwa mengi kuliko yao; hivyo umetokeza, ya kuwa dada zako ni waongofu kuliko wewe kwa ajili ya machukizo yako yote, uliyoyafanya. Basi, wewe nawe shikwa na soni mwenyewe kama dada zako, ulipowaumbua! Kwa hivyo, ulivyokosa na kufanya machukizo kuliko wao, wameonekana kuwa waongofu kuliko wewe. Kwa hiyo wewe nawe iva uso kwa kushikwa na soni ikupasayo, kwa kuwa umewatokeza dada zako kuwa waongofu. Itakuwa, nitakapoyafungua tena mafungo yao: mafungo ya Sodomu na ya wanawe wa kike nayo mafungo ya Samaria na ya wanawe wa kike, kisha nayo mafungo yako wewe, uwe katikati yao, kusudi upate kushikwa na soni ikupasayo; ndipo, utakapoona soni kweli kwa ajili yao yote, uliyoyafanya na kuwapatia wale matulizo ya mioyo yao. Hapo dada zako Sodomu na wanawe watakapokuwa tena, kama walivyokuwa kale, naye Samaria na wanawe watakapokuwa tena, kama walivyokuwa kale, ndipo, wewe nawe na wanao mtakapokuwa, kama mlivyokuwa kale. Je? Jina lake dada yako mdogo Sodomu halikuwa kinywani mwako la kutishia siku zile, ulipokuwa mwenye majivuno? Ni hapo, mabaya yako yalipokuwa hayajafunuliwa bado, kama yalivyofunuka siku zile, wanawake wa Ushami walipokutukana pamoja nao wote wanaokaa na kukuzunguka, ndio wanawake wa Wafilisti waliokubeza po pote. Hivyo ndivyo, ulivyotwikwa uzinzi wako na machukizo yako; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Ninakufanyizia, kama wewe ulivyofanya; kiapo ulikibeua, ukalivunja agano. Lakini mimi nitalikumbuka agano, nililolifanya na wewe siku zile za utoto wako, nikusimikie agano la kale na kale. Ndipo, utakapozikumbuka njia zako na kuona soni utakapowachukua dada zako walio wakubwa kuliko wewe nao walio wadogo kuliko wewe, nitakapowatoa, nikupe wawe wanao, lakini sitavifanya kwa ajili ya agano lako. Ndipo, mimi nitakapolisimika lile agano, nitakalolifanya na wewe, upate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana. Itakuwa hivyo, kusudi uyakumbuke hayo na kuiva uso, usikifumbue kinywa chako tena kwa ajili ya soni, utakayoiona, mimi nitakapokupoza kwa ajili yao yote, uliyoyafanya; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, utegee mlango wa Isiraeli kitendawili na kuuambia fumbo! Sema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kulikuwako tai mkubwa mwenye mabawa makubwa na manyoya marefu mabawani ya kumwendesha, nayo mengi mno yalikuwa yenye rangi; huyo akaja Libanoni, akajichukulia kilele cha mwangati. Chipuko lake la juu penyewe akalivunja, akalipeleka katika nchi yenye biashara, akalitia mjini, wachuuzi wakaamo. Kisha akachukua nayo mbegu ya hiyo nchi, akaipanda shambani panapopandwa mbegu, kwenye maji mengi, iwe kijiti, akaitunza kama mbula. Ikaota, ikawa mzabibu uliotambaa wenye kisiki kifupi, kwani matawi yake yalimgeukia mwenyewe, nayo mizizi yake ilikuwa chini yake yeye; ukawa mzabibu wa kweli, ukapata matawi yaliyochipuza majani mazuri. Kukawa na tai mkubwa mwingine mwenye mabawa makubwa yenye manyoya mengi; mara ule mzabibu ukampindukia yeye, mizizi yake imtwetee kwa kumtamani, nayo matawi yake ukamwelekezea yeye, aunyweshe kuliko hayo matuta, ulikopandwa. Nao ulikuwa umepandwa katika shamba zuri lenye maji mengi, uchipuke matawi yatakayoleta matunda, uwe mzabibu wenye utukufu. Basi, sema: hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Je? Utafanikiwa? Yule hataing'oa mizizi yake na kuyakata matunda yake, ukauke? Kweli majani yote ya machipuko yake yatakauka; hautatakiwa mkono wenye nguvu wala watu wengi wa kuung'oa kwenye mizizi yake. Kweli ulikuwa umepandwa, lakini utafanikiwa? Hautakauka kabisa, upepo utokao upande wa maawioni kwa jua utakapouvumia? Utakauka kweli hapo hapo matutani, ulikochipukia. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Uambie mlango huu mkatavu: Je? Hamwijui maana yake hayo? Sema: Mwemwona mfalme wa Babeli, akija Yerusalemu, akimchukua mfalme wake na wakuu wake na kuwapeleka kwake Babeli. Kisha alichukua mmoja wa kizazi cha kifalme, akafanya naye agano na kumwapisha. Lakini wenye nguvu wa nchi hii akawachukua, ufalme ukae chini tu, usijikweze, usimamike tu kwa kulishika agano lake. Kisha huyo akakataa kumtii, akatuma wajumbe kwenda Misri, wampe farasi na watu wengi. Aliyeyafanya hayo atawezaje kufanikiwa na kujiokoa? Kwa kulivunja agano ataponaje? Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, kweli atakufa mle Babeli, mle mjini, mfalme akaamo aliyempa ufalme, kwa kuwa alikibeza kiapo chake na kulivunja agano lake. Naye Farao hataleta vikosi vikubwa vyenye watu wengi amfalie kitu vitani, watakapomzungushia ukingo wa mchanga na kujenga minara, kusudi waangamize watu wengi na kuwaua. Kwa kuwa alikibeua kiapo na kulivunja agano, aliloliinulia mkono, kwa hiyo ataona: kwa kuyafanya hayo yote hataokoka. Kwa sababu hii ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, kiapo changu alichokibeua, na agano langu, alilolivunja, nitamtwika kichwani. Nami nitamtegea wavu wangu, anaswe katika tanzi langu kisha nitampeleka Babeli; ndiko, nitakakomkatia shauri kwa kuyavunja maagano yangu. Nao watoro wake wote katika vikosi vyake vyote wataangushwa kwa panga, nao watakaosalia watatawanywa pande zote za upepo. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi Bwana nimesema. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mimi nitachukua tawi la kilele cha mwangati mrefu, nilipande; pake juu penyewe katika mlima mrefu ulioinuka sana. Katika huo mlima mrefu wa Isiraeli nitalipanda, lichupuke matawi yatakayozaa mbegu, nalo litakuwa mwangati wenye utukufu; chini yake watakaa ndege wa kila namna wenye manyoya mbalimbali, chini kivulini mwa matawi yake watajenga matundu yao. Ndipo, miti yote ya shambani itakapojua, ya kuwa mimi Bwana hunyenyekeza mti mrefu, tena hukuza mti mfupi, ya kuwa mimi hukausha mti mbichi, tena huchipuza mti mkavu. Mimi Bwana niliyeyasema nitayafanya. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Ninyi hulitumiaje katika nchi ya Isiraeli fumbo kama hilo la kwamba: Baba walipokula zabibu bichi, ndipo, wana alipokufa ganzi la meno. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, hatakuwako tena kwenu atakayelitumia fumbo hili kwao Waisiraeli. Tazameni: Roho zote za watu ni zangu, kama ni roho za baba, au kama ni roho za wana, zote ni zangu; roho ya mtu atakayekosa ndiyo itakayokufa. Mtu akiwa mwongofu, afanye yaliyo sawa yaongokayo, asile vilimani juu, wala asiyatazamie kwa macho yake magogo ya kutambikia ya mlango wa Isiraeli, wala asimchafue mke wa mwenziwe, wala asimkaribie mwanamke mwenye siku zake, wala asimtese mtu, ila aliyemkopa amrudishie aliyompa yeye ya kumwekea, asinyang'anye isiyo mali yake, wenye njaa awagawie vyakula vyake, wenye uchi awavike nguo, asikopeshee kupata faida, wala asichukue nyongeza za kupunja, mkono wake auzuie, usipotoe, aamue kwa kweli, mtu akigombana na mwenziwe, ayafuate maongozi yangu na kuyashika mashauri yangu na kufanya yaliyo kweli, basi, mtu aliye hivyo ni mwongofu, naye atapata uzima wa kweli; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Mtu kama huyo akizaa mwana aliye mkorofi, amwage damu, afanye moja tu la mabaya yale, yeye baba yake asiyoyafanya yote, kama anakula vilimani juu, au kama anamchafua mke wa mwenziwe, au kama anawatesa wanyonge na wakiwa, au kama ananyang'anya mali yake, au kama harudishi aliyopewa ya kumwekea mtu, au kama anayatazamia kwa macho yake magogo ya kutambikia, ayafanye yachukizayo, au kama anakopeshea kupata faida, au kama anachukua nyongeza za kupunja, basi, yeye atapata kabisa uzima wa kweli, ila atakufa kweli kwa kuyafanya hayo machukizo yote akitwikwa manza zake za damu, alizozikora. Huyu akizaa mwana, naye akiyaona makosa yote, baba yake aliyoyatenda, lakini akiyaona tu, asiyafanye yaliyo kama hayo, asile vilimani juu, wala asiyatazamie kwa macho yake magogo ya kutambikia ya mlango wa Isiraeli, wala asimchafue mke wa mwenziwe, wala asimtese mtu, wala asimtoze mtu mali za kumwekea, wala asinyang'anye isiyo mali yake, ila wenye njaa awagawie vyakula vyake, wenye uchi awavike nguo, auzuie mkono wake, usipotoe mnyonge, wala usichukue faida wala nyongeza za kupunja, ayafanye mashauri yangu na kuyafuata maongozi yangu, basi aliye hivyo hata kufa kwa ajili ya manza, baba yake alizozikora, ila atapata uzima wa kweli. Lakini baba yake aliyekorofisha kwa ukorofi wake, aliyemnyang'anya ndugu mali isiyo yake, aliyefanya katikati ya wenziwe wa ukoo yasiyo mema, mtamwona, yeye akifa kwa ajili ya hizo manza, alizozikora. Mkiuliza: Sababu gani mwana hatwikwi naye manza za baba yake? ni hivyo: mwana alifanya yaliyo sawa yaongokayo, akayashika maongozi yangu yote na kuyafanya, kwa hiyo atapata uzima wa kweli. Roho ya mtu atakayekosa ndiyo itakayokufa, lakini mwana hatatikwa manza za baba yake, wala baba hatatwikwa manza za mwanawe, nao wongofu wake mwongofu utamkalia, nao ubezi wake asiyemcha Mungu utamkalia. Lakini asiyemcha Mungu akirudi na kuyaacha makosa yake yote, aliyoyafanya, ayashike maongozi yangu yote na kufanya yaliyo sawa yaongokayo, basi, atapata uzima wa kweli, hatakufa. Nayo mapotovu yake yote, aliyoyafanya, hayatakumbukwa, ila atapata uzima kwa wongofu wake, alioufanya. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Mnaniwaziaje kwamba: Nitapendezwa, asiyenicha akifa? Je? Sitapendezwa, akirudi na kuziacha njia zake, apate uzima? Lakini mwongofu akigeuka na kuuacha wongofu wake, afanye mapotovu, ayafanye hayo machukizo yote, wasiomcha Mungu wanayoyafanya, je? Atapata uzima? Sivyo, wongofu wote, alioufanya, hautakumbukwa, kwa kuwa amevunja maagano, naye kwa ajili ya makosa yake, aliyoyakosa, atakufa. Mkisema: Kumbe njia ya Bwana hainyoki! Sikieni, ninyi wa mlango wa Isiraeli: Je? Njia yangu hainyoki? Sizo njia zenu zisizonyoka? Mwongofu akirudi na kuuacha wongofu wake, afanya maovu, atakufa kwa ajili yao, kweli, kwa ajili ya hayo maovu, aliyoyafanya, atakufa. Tena asiyemcha Mungu akirudi na kumcha Mungu afanye yaliyo sawa yaongokayo, huyu ataipatia roho yake uzima. Akipata kuona, akirudi na kuyaacha mapotovu yake yote, aliyoyafanya, atapata uzima wa kweli, hatakfufa. Wao wa mlango wa Isiraeli wakisema: Njia ya Bwana hainyoki, inakuwaje, njia zangu zisiponyoka? Ninyi wa mlango wa Isiraeli, sizo njia zenu zisizonyoka? Kwa hiyo nitawapatiliza ninyi wa mlango wa Isiraeli kila mtu, kama njia zakezilivyo; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Rudini na kujigeuza na kuyaacha mapotovu yenu yote, yasiwawie tena makwazo ya kuwakosesha! Yatupeni mapotovu yenu yote mliyoyafanya ya kuwapotoa wenzenu, yawatoke ninyi! Kisha jipatieni mioyo mipya! na roho mpya! Mbona mnataka kufa, ninyi wa mlango wa Isiraeli? Kweli sipendezwi na kufa kwake mwenye kufa; ndivyo asemavyo Bwana Mungu. Kwa hiyo jigeuzeni, mpate uzima! Basi, tunga ombolezo la kumwombolezea mkuu wa Isiraeli! Sema: Mama yako alikuwa nani? Simba mke! Alilala kwenye masimba, kwenye wana wa simba katikati aliwakuza wanawe. Hao wanawe mmoja wao, alipokwisha kumlea, akawa kijana wa simba, akajifunza kunyafua nyama, aliowakamata, akala nao watu. Wamizimu walipoyasikia, walimchimbia mwina, akanaswa humo, wakamtia pete puani, wakampeleka katika nchi ya Misri. Mama yake alipoona, ya kuwa alimngojea bure, kingojeo chake kikapotea; kisha akachukua mwingine katika wanawe, akamtunza, awe kijana wa simba. Akajiendea kwenye masimba kati, akawa kijana wa simba, akajifunza kunyafua nyama aliowakamata, akala nao watu. Akayajua majumba yao, akaiangamiza miji yao, nchi akaigeuza kuwa peke yake tu, waliojaa huko wakitoweka kwa kuziogopa sauti za ngurumo zake. Ndipo, wamizimu walipotoka katika nchi zao, wakajipanga na kumzunguka, wakamtegea nyavu zao, wakamchimbia nao mwina, akanaswa humo. Kisha wakamtia pete puani, wakamtia katika tundu kubwa, wakampeleka kwa mfalme wa Babeli, wakampeleka kweli, mpaka wakamweka bomani, kusudi sauti zake zisisikilike tena katika miji ya Isiraeli. Mama yako alikuwa kama mzabibu shambani kwa mizabibu yako uliopandwa penye maji, ukazaa matunda, ukawa na matawi mengi, kwani ulikuwa penye maji mengi. Ukapata hata fimbo zenye nguvu zilizofaa kuwa bakora za watawala nchi, ukawa mrefu kwa kimo chake, ukayapita majani ya miti iliyoko, ukaonekana mbali kwa urefu wake na kwa wingi wa matawi yake. Kisha ukang'olewa kwa makali yenye moto, ukatupwa chini, upepo uliotoka maawioni kwa jua ukayanyausha matunda yake, matawi yake yenye nguvu yakavunjwa, yakakauka, kisha moto ukayala. Kisha ukapandwa nyikani katika nchi kavu yenye kiu. Moto ukatoka katika zile fimbo za matawi yake, ukayala matunda yake, haikuwako tena kwake fimbo yenye nguvu iliyofaa kuwa bakora ya mtawala nchi. Hili ndilo ombolezo litakalokuwa ombolezo kweli. Ikawa katika mwaka wa 7 mwezi wa tano siku ya kumi, ndipo waume wazee wa Kiisiraeli walipokuja kumwuliza Bwana, wakakaa mbele yangu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, sema na wazee wa Kiisiraeli, uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Inakuwaje, mkija kuniuliza? Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, siulizwi nanyi! ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Haitafaa, ukiwahukumu wewe? Je? Haitafaa ukiwahukumu wewe, mwana wa mtu? Wajulishe machukizo ya baba zao! Waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Siku ile, nilipowachagua Waisiraeli, niliuinua mkono wangu na kuwaapia walio uzao wa mlango wa Yakobo, nikajijulisha kwao katika nchi ya Misri, nikauinua mkono wangu na kuwaapia kwamba: Mimi ni Bwana Mungu wenu. Siku ile niliuinua mkono wangu na kuwaapia, ya kuwa nitawatoa katika nchi ya Misri na kuwapeleka katika nchi, niliyowachagulia kuwa nchi ichuruzikayo maziwa na asali, tena kuwa nchi iliyo urembo wa nchi zote. Ndipo, nilipowaambia: Yatupeni kila mtu hayo yatapishayo kwa kutazamwa tu! Msijipatie uchafu kwa kuyatambikia magogo yao Wamisri ya kutambikia! Mimi Bwana ni Mungu wenu. Kisha wakanikataa wasipotaka kunisikia, hawakuyatupa kila mtu matapisho yake aliyoyatazama, wala hawakuyaacha magogo yao Wamisri ya kutambikia, nikasema: Nitawamwagia makali yangu yenye moto, machafuko yangu yamalizike kwao kulekule katika nchi ya Misri. Lakini nikafanya mengine kwa ajili ya Jina langu, lisitiwe uchafu machoni pao wamizimu, kwani wanakaa wakizungukwa nao, nami nilijijulisha machoni pao kwamba: Nitawatoa katika nchi ya Misri. Basi, nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawapeleka nyikani. Nikawapa maongozi yangu, nikawajulisha nayo mashauri yangu, nayo ndiyo yatakayompa mtu uzima, akiyafanya. Nikawapa nazo siku zangu za mapumziko, ziwe kielekezo cha maagano, tuliyoyaagana mimi nao, wajue, ya kuwa mimi ni Bwana awatakasaye. Lakini walio mlango wa Isiraeli wakanikataa nako nyikani: maongozi yangu hawakuyafuata, mashauri yangu wakayabeza, nayo ndiyo yatakayompa mtu uzima, akiyafanya. Nazo siku zangu za mapumziko wakazipitia uchafu sana, nikasema: Nitawamwagia makali yangu yenye moto huku nyikani, yawamalize. Lakini nikafanya mengine kwa ajili ya Jina langu, lisitiwe uchafu machoni pao wamizimu walioona kwa macho yao, jinsi nilivyowatoa. Nami nikauinua mkono wangu na kuwaapia huko nyikani kwamba: Sitawapeleka katika nchi ile, niliyowapa, ichuruzikayo maziwa na asali, iliyo urembo wa anchi zote, kwa kuwa waliyabeza mashauri yangu, hawakuyafuata maongozi yangu, wakazipatia siku zangu za mapumziko uchafu, kwani mioyo yao ikayaendea magogo yao ya kutambikia. Lakini macho yangu yakawaonea uchungu, nisiwaangamize; basi, nikaacha kuwamaliza nyikani. Nikawaambia wana wao huko nyikani: Maongozi ya baba zenu msiyafuate, wala msiyashike mashauri yao, wala msijichafue kwa kuyatambikia magogo yao! Mimi Bwana ni Mungu wenu, yafuateni maongozi yangu! Yashikeni nayo mashauri yangu, myafanaye! Zitakaseni siku zangu za mapumziko, ziwe kielekezo cha maagano, tuliyoyafanya mimi nanyi, mjue, ya kuwa mimi ni Mungu wenu! Lakini hao wana nao wakanikataa: maongozi yangu hawakuyafuata, mashauri yangu hawakuyashika, wayafanye, nayo ndiyo yatakayompa mtu uzima, akiyafanya; siku zangu za mapumziko wakazipatia uchafu, nikasema: Nitawamwagia makali yangu yenye moto, machafuko yangu yamalizike kwao nyikani. Kisha nikaurudisha mkono wangu, nikafanya mengine kwa ajili ya Jina langu, lisitiwe uchafu machoni pao wamizimu walioona kwa macho yao, jinsi nilivyowatoa. Nami nikauinua mkono wangu na kuwaapia huko nyikani kwamba: Nitawatawanya kwenye wamizimu na kuwatupatupa katika nchi zao, kwa kuwa hawakuyafanya mashauri yangu, wakayabeza maongozi yangu, wakazipatia siku zangu za mapumziko uchafu, wakayatazamia kwa macho yao magogo, baba zao waliyoyatambikia. Ndipo, mimi nami nilipowatolea maongozi yasiyokuwa mema, hata amashauri yasiyoweza kuwapa uzima. Nikawapatia uchafu kwa vipaji vyao vya tambiko, wakawapitisha motoni wote waliofungua tumbo la mama, kusudi niwastushe, wajue, ya kuwa mimi ni Bwana. Kwa hiyo sema na mlango wa Isiraeli, wewe mwana wa mtu, uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Hata kwa neno hili baba zenu walinitukana, wakilivunja agano. Nilipokuwa nimekwisha kuwapeleka katika nchi, niliyowaapia kwa kuuinua mkono wangu kwamba: Nitawapa basi, po pote walipoona kilima kirefu, napo walipoona mti wenye majani mengi, ndipo, walipochinja ng'ombe zao za tambiko, wakatoa hapohapo vipaji vyao vya tambiko, kusudi wanikasirishe, wakavukiza hapo uvumba wao wenye mnuko wa kupendeza, wakamwagia hapo vinywaji vyao vya tambiko. Nikawauliza: Kiko kilima gani, mnachokijia hapo? Kwa hiyo jina lake likaitwa Kilima hata siku ya leo. Kwa hiyo uambie mlango wa Isiraeli: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Je? Mnajipatia uchafu kwa kuzishika njia za baba zenu? Je? Nanyi mnafanya ugoni kwa kuyafuata matapisho yao? Hata kwa kutoa vipaji vyenu vya tambiko, mkiwapitisha wana wenu motoni, mnajipatia uchafu na kuyatumikia magogo yenu yote ya kutambikia mpaka siku ya leo, sasa je? Mimi niulizwe nanyi mlio mlango wa Isiraeli? Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo nilivyo Mwenye uzima, sitaulizwa nanyi kabisa! Nayo yanayowazwa rohoni mwenu hayatakuwa kabisa, ninyi mkisema: Nasi na tuwe, kama wamizimu nao wa koo za nchi hizi walivyo, tukitumikia miti na mawe. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, mimi nitakuwa mfalme wenu kwa kiganja chenye nguvu na kwa mkono ukunjukao na kwa makali yenye moto yamwagwayo. Nami nitawatoa kwenye makabila mengine nikiwakusanya na kuwatoa katika nchi hizi, mlikotupwa kwa kiganja chenye nguvu na kwa mkono ukunjukao na kwa makali yenye moto yamwagwayo. Nitawapeleka katika nyika ya makabila mengine; ndiko, nitakakowakatia mashauri uso kwa uso. Kama nilivyowakatia baba zenu shauri katika nyika ya Misri, ndivyo, nitakavyofanya shauri nanyi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Nitawapitisha chini ya fimbo ya uchungaji, nije kuwashurutisha kulishika agano. Nitatenga kwenu wakatavu nao walionikosea, nikiwatoa katika nchi wakaako ugeni, wasiingie nchi ya Waisiraeli; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Tena kwa ajili yenu mlio mlango wa Isiraeli Bwana Mungu anasema hivi: Haya! Nendeni kila mtu kuyatumikia magogo yenu ya kutambikia! Lakini siku za nyuma mtanisikiliza kabisa, msilitie jina la Patakatifu pangu tena uchafu kwa vipaji vyenu vya tambiko na kwa magogo yenu ya kutambikia. Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Katika mlima wangu mtakatifu utakaokuwa mlima mrefu wa Isiraeli ndiko, watakakonitumikia wao wa milango yote ya Isiraeli nazo nchi zake zote; tena ndiko, nitakakowapendeza nikitaka kuvipokea vipaji vyenu, mtakavyonitolea, nayo malimbuko yenu ya kunitambikia katika yote, mtakayonitakasia. Hapo nitawapendeza na kuutaka mnuko mzuri, nitakapowatoa kwenye makabila mengine na kuwakusanya, mzitoke hizo nchi, mlikotawanywa; ndipo, nitakapotakaswa kwenu machoni pao wamizimu. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nikiwapeleka katika nchi ya Isiraeli, katika ile nchi niliyowaapia na kuuinua mkono wangu kwamba: Nitawapa baba zenu. Nanyi huko mtazikumbuka njia zenu na matendo yenu, mliyojipatia uchafu nayo, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya mabaya yenu yote, mliyoyafanya. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapowafanyizia hivyo kwa ajili ya Jina langu, lakini sivyo kwa ajili ya njia zenu mbaya, wala kwa ajili ya matendo yenu maovu, ninyi wa mlango wa Isiraeli; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, uelekeze uso wako kutazama upande wa kusini, uitangazie nchi yenye jua kali, ukiufumbulia mwitu ulioko kwenye mbuga za kusini yatakayokuwa. Uuambie huo mwitu ulioko kusini: Lisikie neno la Bwana! Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaona, nikiwasha moto kwako utakaokula kwako miti mibichi yote na miti mikavu yote; miali ya moto huo uwakao haitazimika, mpaka nyuso zote toka kusini hata kaskazini ziunguzwe nao. Ndipo, wote wenye miili watakapoona ya kuwa mimi ni Bwana, ya kuwa mimi nimewasha moto usiozimika. Nikasema: E Bwana Mungu, hao hunisema kwamba: Yeye siye atumiaye mafumbo? Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, uelekeze uso wako kuutazama Yerusalemu, upatangazie Patakatifu na kuifumbulia nchi ya Isiraeli yatakayokuwa! Iambie nchi ya Isiraeli: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Utaona, nikikujia na kuuchomoa upanga wangu alani mwake, niangamize waongofu na wapotovu, watoweke kwako. Kwa kuwa nitaangamiza waongofu na wapotovu, watoweke kwako, kwa hiyo upanga wangu utachomolewa alani mwake, uwapige wote wenye miili toka kusini hata kasikazini. Ndipo, wote wenye miili watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, ya kuwa nimeuchomoa upanga wangu alani mwake, usirudi humo tena. Lakini wewe mwana wa mtu, piga kite! Kwa viuno vilivyovunjika na kwa uchungu ulio mkali piga kite, wakuone! Tena wakikuuliza: Unapiga kite? uwaambie: Kwa hayo, niliyoyasikia, ya kuwa yatakuja, moyo wote umeyeyuka, nayo mikono ikalegea, nayo roho yote ikazimia, nayo magoti yakaja kugeuka kuwa kama maji. Mtaona, yakija kutimia; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, yafumbue yatakayokuwa ukisema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Sema: Uko upanga, ni upanga mwenyewe, umenolewa na kusuguliwa vema. Umenolewa, kusudi uchinje machinjo, ukasuguliwa, kusudi ukatuke kama umeme. Au tuufurahie? Fimbo ya kumpigia mwanangu haishindwi na mti wo wote. Aliutoa, usuguliwe vema, apate kuushika mkononi; nao ukanolewa ule upanga, ukasuguliwa vema, mwuaji apewe mkononi. Piga yowe na kupaza sauti, mwana wa mtu! Kwani huo ndio unaowajia walio ukoo wangu, ndio unaowajia nao wakuu wa Isiraeli; wametupwa kwenye upanga pamoja nao walio ukoo wangu. Kwa hiyo jipige mapaja! Kwani walijaribiwa, lakini imewafaliaje? Sasa je? Fimbo nayo ikatae kuwapiga? Haitakuwa; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Nawe mwana wa mtu, yafumbue yatakayokuwa ukiyapiga makofi! Kwani huo upanga utakuja mara mbili, hata mara tatu, ndio upanga upigao madonda kabisa, kweli ndio upanga mkubwa upigao madonda, ndio utakaowazunguka, kusudi mioyo iyeyuke, tena wengi waanguke kwa kukwazwa; malangoni pao po pote nitatoa matisho ya huo upanga. A! Umefanywa, umerimete kama umeme! Umenolewa, upate kuchinja! Jitege kupiga kuumeni! Jiweke tayari kupiga kushotoni! Piga po pote, makali yako yatakapoelekea! Mimi nami nitayapiga makofi yangu nitakapoyatuliza makali yangu yenye moto; mimi Bwana nimeyasema. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Wewe mwana wa mtu, jitengenezee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli utakazozishika! Zote mbili zitatoka katika nchi moja; hapo njia pembeni pachore mkono, uelekezee mji, ndivyo uuchore! Tengeneza njia, upanga utayoishika kwenda Rabati ya wana wa Amoni, tena nyingine kwenda Yuda katika Yerusalemu ulio na boma. Kwani mfalme wa Babeli atasimama hapo penye njia panda, zile njia mbili zinapoanzia, apate kuagua uaguaji, akisukasuka mishale au akipiga bao au akitazama maini. Kuumeni kwake kutaanguka kura ya Yerusalemu kwamba: aweke magogo ya kuvunjia boma, afumbue kinywa kupiga kelele, apaze sauti kupiga yowe, aweke magogo ya kuvunjia penye malango, azungushe ukingo wa mchanga, ajenge minara. Nao uaguaji kama huo utakuwa uwongo machoni pao, ijapo wauapie viapo; lakini yeye atawakumbusha manza, walizozikora, kusudi watekwe. Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Kwa kuwa mnanikumbusha manza, mlizozikora, mapotovu yenu yakifunuliwa, makosa yenu yakitokea waziwazi kwa matendo yenu yote, kwa kuwa mnakumbukwa hivyo, basi, mtakamatwa kwa mikono. Lakini wewe mkuu wa Isiraeli uliyejipatia uchafu kwa kuacha kunicha, siku yako imetimia, kwa kuwa ni wakati wa mwisho wa kukora manza. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kiondoe kilemba cha kifalme! Ivue nayo taji! Haya ya sasa siyo yatakayokuwa tena. Yaliyoko chini ndiyo, watakayoyakweza, nayo yaliyoko juu ndiyo, watakayoyanyenyekeza. Mabomoko na mabomoko na mabomoko ndiyo, nitakayoyaweka huku; lakini nayo siyo yatakayokuwa vivyo hivyo, mpaka aje, ambaye ni haki yake; yeye ndiye, nitakayempa. Nawe mwana wa mtu, yafumbue yatakayokuwa ukisema: Haya ndiyo Bwana Mungu anayowaambia wana wa Amoni kwa ajili ya matusi yao, sema: Upanga ulio upanga kweli umechomolewa, nao umesuguliwa, upate kuchinja na kuua kabisa, kusudi uwe kama umeme. Lakini wamekutazamia maono yasiyokuwa, wakakuagulia uwongo, wakuvute, uje kuwapiga shingo zao waliojipatia uchafu na kuacha kunicha, kwamba siku yao imetimia, kwa kuwa ni wakati wa mwisho wa kukora manza. Lakini urudishe huo upanga alani mwake! Mahali, ulipoumbwa katika nchi, ulikozaliwa, nitakukatia shauri. Nitakumwagia makali yangu, kwa moto wa machafuko yangu nitakufokea, kisha nitakutia mikononi mwa watu wasio wa kimtu, walio mafundi wa maangamizo. Utakuwa chakula cha moto, damu yako itamwagwa katika nchi yako katikati, hutakumbukwa tena, kwani mimi Bwana nimeyasema. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Wewe mwana wa mtu, hutauhukumu, kweli hutauhukumu mji huo ujaao damu za watu? Uujulishe machukizo yake yote! Sema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wewe ndiwe mji uliomwaga mwake damu za watu, siku zake zitimie, ukafanya magogo ya kutambikia, ukajipatia uchafu nayo. Kwa hizo damu zako, ulizozimwaga, umekora manza, tena kwa hayo magogo ya kutambikia, uliyoyafanya, umejipatia uchafu, hivyo umezifikisha siku zako karibu, ukaja penye mwisho wa miaka yako. Kwa hiyo nitakutia soni kwa wamizimu, usimangwe katika nchi zote. Nchi zilizoko karibu yako nazo zilizoko mbali yako zitakusimanga kwamba: Umelipatia jina lako uchafu, ukafanya matata mengi. Tazama, wakuu wa Isiraeli wote walikuwa mwako wakiitumia mikono yako kumwaga damu za watu. Mwako watu hawachi wala baba wala mama, nao wageni huwafanyia ukorofi mwako, wafiwao na wazazi nao wajane watu huwatesa mwako. Patakatifu pangu wewe hupabeza, nazo siku zangu za mapumziko wewe huzichafua. Mwako mna watu wanaowaonea wenzao, wapate kumwaga damu zao, tena mwako wamo wanaokula vilimani vyakula vya tambiko, hata uzinzi watu hufanya mwako. Yenye soni ya baba watu huyafunua mwako, mwako huwatumia kwa nguvu nao wanawake wenye uchafu kwa kuwa na siku zao. Wako wanowafanyizia wake wa wenzao yachukizayo, tena wako wanojichafua kwa kuwatumia wakwe wao wa kike kufanya uzinzi nao, tena wako wanaowatumia kwa nguvu nao maumbu zao waliozaliwa na baba yao. Mwako wamo wanotaka kupenyezewa fedha, kusudi wamwage damu, tena huchukua faida na nyongeza za kupunja, mkiwadanganya wenzenu kwa ukorofi, lakini mimi mmenisahau; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Lakini utaniona, nikiyapiga makofi yangu kwa ajili ya mali zako, ulizojipatia kwa udanganyifu, na kwa ajili ya damu zako zilizomwagwa mwako mjini katikati. Je? Moyo wako utasimama? Je? Mikono yako itakuwa na nguvu zao siku zile, nitakapokufanyizia mambo? Mimi Bwana nimeyasema, nami nitayafanya. Nitakutawanya kwa wamizimu na kukutupatupa katika nchi zao; hivyo nitaukomesha uchafu wako kabisa, uishe kwako! Nawe utakuwa mwenye upujufu machoni pao wamizimu; ndipo, utakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, walio mlango wa Isiraeli wameniwia kama mavi ya chuma, wao wote ni kama shaba nyekundu na shaba nyeupe na chuma na risasi katika tanuru, wamegeuka kuwa mitapo ya fedha. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa ninyi nyote mmegeuka kuwa mitapo ya fedha, mtaniona, nikiwakusanya ninyi mjini mwa Yerusalemu; kama fedha na shaba nyekundu na chuma na shaba nyeupe zinavyokusanywa ndani ya tanuru, ziwashiwe moto, zipate kuyeyuka, hivyo ndivyo, nitakavyowakusanya kwa makali yangu na kwa machafuko yangu yenye moto, niwatie mle ndani kuwayeyusha. Kweli nitawakusanya, niwawashie moto wa machafuko yangu; ndivyo, nitakavyowayeyusha mle ndani. Kama wanavyoyeyusha fedha ndani ya tanuru, ndivyo mtakavyoyeyushwa ndani yake. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nimewamwagia makali yangu yenye moto. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, iambie nchi hii: Wewe ndiwe nchi isiyotakasika, isiyonyweshwa mvua siku ya kukasirikiwa. Wafumbuaji wake waliomo mwake wamekula njama, wakawa kama simba angurumaye akinyafua nyama, aliowakamata; nao wakazila roho za watu, wakazitwaa nazo mali zao na vitu vyao vyenye kiasi, wakawaua waume wao wanawake wengi waliokuwamo, wakawageuza kuwa wajane. Watambikaji wao wakayapotoa Maonyo yangu, wakapachafua Patakatifu pangu hawakuyapambanua matakatifu nayo yatumiwayo tu, wala hawakuyajulisha watu kuyapambanua yaliyo machafu nayo yaliyotakata, tena wameyafumba macho yao penye siku zangu za mapumziko nikapatiwa uchafu katikati yao. Wakuu wao waliokuwa mle mjini wakawa kama chui wanaonyafua nyama waliowakamata, hutaka kumwaga damu za watu na kuziangamiza roho zao, kusudi wajipatie mali za madanganyo yao. Nao wafumbuaji wake huyapaka mambo yao yote chokaa, wakiona maono ya uwongo na kusema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema, naye Bwana hakusema neno. Watu wa nchi hii hukorofisha kabisa na kupokonya sana, hutesa wanyonge na wakiwa, hukorofisha nao wageni kwa njia zisizonyoka. Nikatafuta mtu wa kwao afaaye kuujenga ukuta na kusimama mbele yangu palipoatuka ufa, aikingie nchi hii, nisiiangamize, lakini sikumwona. Nikawamwagia makali yangu nikawamaliza kwa moto wa machafuko yangu, nikawatwika njia zao vichwani pao; ndivyo asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, kulikuwako wanawake wawili waliozaliwa na mama yao mmoja. Wakafanya ugoni katika nchi ya Misri; wangaliko wasichana bado, walifanya ugoni. Huko wakapenda kushikwashikwa vifua vyao na kubanwabanwa maziwa ya uwanawali wao. Majina yao mkubwa aliitwa Ohola (Hema lake) naye nduguye Oholiba (Hema langu limo mwake); wakawa wangu, wakazaa wana wa kiume na wa kike. Nayo hayo majina yao lile la Ohola lilikuwa la Samaria, nalo la Oholiba lilikuwa la Yerusalemu. Ohola akafanya ugoni alipokuwa ni wangu, akawatamani wapenzi wake Waasuri waliomkaribia. Walikuwa wamevaa nguo za kifalme za rangi nyeusi; nao walikuwa watawala nchi na wakuu, wote walikuwa vijana wa kutamaniwa kwa kupendeza, wakaja wakichukuliwa na farasi, hao farasi ndio waliopandwa nao. Hao ndio, aliojitolea kwa ugoni wake, kwani wote walikuwa vijana wateule wa wana wa Asuri, kwao wote, aliowatamani, akajipatia uchafu na kuyatumikia magogo yao ya kutambikia. Nao ugoni wake, alioufanya Misri, hakuuacha; kwani wao walilala kwake, alipokuwa msichana bado, nao ndio walioyabanabana maziwa ya uwanawali wake wakimmwagia ugoni wao. Kwa hiyo nimemtia mikononi mwao wapenzi wake, ndimo mikononi mwa wana wa Asuri, aliowatamani, Nao waliyafunua yake yenye soni, wakawachukua wanawe wa kiume nao wa kike, naye mwenyewe wakamwua kwa upanga. Kisha jina lake likatumiwa kwa wanawake kuwa tisho, alipokuwa amekwisha kuhukumiwa. Ijapo nduguye Oholiba alikuwa ameyaona, akauzidisha ubaya wa tamaa zake kuliko yule, nao ugoni wake ukazidi kuliko ugoni wake yule. Akawatamani wana wa Asuri, watawala nchi na wakuu wakamkaribia wakiwa wamevaa nguo za urembo kabisa, nao wakaja wakichukuliwa na farasi, hao farasi ndio waliopandwa nao, wao wote walikuwa vijana wa kutamaniwa kwa kupendeza. Nikamwona, alivyochafuliwa. Hao wawili njia yao ilikuwa moja tu. Naye huyu akaendelea kwa ugoni wake, alipoona waume waliochorwa ukutani, ni sanamu za Wakasidi zilizochorwa mle na kutiwa rangi nyekundu. Walikuwa wamejifunga ukanda viunoni pao, vichwani pao walikuwa wamejifunga vilemba vya nguo za rangi vipana sana, sura zao wote walionekana kuwa wapanda magari ya vita, walifanana nao wana wa Babeli; ndiko, hao wakasidi walikozaliwa. Akawatamani alipowaona kwa macho yake, akatuma wajumbe kwenda kwao katika nchi ya wakasidi. Ndipo, wana wa Babeli walipokuja kwake kulala naye kwa kumpenda, wakamtia uchafu kwa ugoni wao; alipokwisha kujipatia uchafu kwao, roho yake ikajitenga nao. Alipoufunua ugoni wake na kuyafunua yake yenye soni, ndipo, roho yangu ilipojitenga naye, kama ilivyojitenga na dada yake. Akauzidisha ugoni wake akizikumbuka siku za ujana wake, alipofanya ugoni katika nchi ya Misri. Akawatamani sana wazinzi wa huko walio wenye miili kama ya punda, nazo tamaa zao za kutokeza mbegu zilikuwa kama za madume ya farasi. Hivyo uliutazamia uzinzi wa ujana wako, wale walioko Misri walipoyabanabana maziwa yako na kuvishikashika vifua vya uwanawali wako. Kwa hiyo, Oholiba, hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikiwaamsha wapenzi wako, wakujie, ambao roho yako ilijitenga nao. Nitawaleta, wakujie toka pande zote: wama wa Babeli na Wakasidi wote, Pekodi na Soa na Koa na wana wote wa Asuri pamoja nao; ndio vijana wa kutamaniwa kwa kupendeza, wote ni watawala nchi na wakuu, wapanda magari ya vita na mabwana wakubwa, wote ni wenye kupanda farasi. Hao watakujia wakileta vyombo vya vita na magari na magurudumu na mikutano ya makabila ya watu wenye ngao kubwa na ngao ndogo na makofia ya vita, kisha watajipanga kwako na kukuzunguka. Nami nitalipeleka shauri lako mbele yao, nao watakukatia shauri, kama wanavyokata mashauri kwao. Kisha nitakutolea wivu wangu, wao wakufanyizie mambo, wayatakayo kwa makali yao yenye moto; watakukata pua na masikio, kisha utauawa kwa upanga. Kisha watawachukua wanao wa kiume na wa kike, nawe wewe mwisho utateketezwa kwa moto. Watakuvua nguo zako wayachukue mapambo yako matukufu. Hivyo nitaukomesha uzinzi wako, uishe kwako pamoja na ugoni wako ulioanzia katika nchi ya Misri, hutaweza tena kuyainua macho yako, uwatazame, wala hutaikumbuka tena nchi ya Misri. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikikutia mikononi mwao, unaowachukia, namo mikononi mwao ambao roho yako ilijitenga nao. Nao watakufanyizia mambo, wayatakayo kwa uchukivu wao, wakiyachukua mapato yako yote kisha watakuacha mwenye uchi pasipo nguo ya kujifunika; ndipo, utakapokuwa umefunuka ugoni wako utiao soni nao uzinzi wako ulio pamoja na ugoni wako. Watakufanyizia hayo, kwa kuwa uliwakimbilia wamizimu, ufanye ugoni nao, tena kwa kuwa ulijipatia uchafu kwa magogo yao ya kutambikia. umeishika njia ya dada yako, kwa hiyo ninakupa kinyweo chake mkononi mwako. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kinyweo cha dada yako utakinywa kilicho kirefu na kipana, uchekwe na kufyozwa! Kwani ni mengi yaliyoenea mle ndani. Ndipo, utakapolewa kabisa na kuona majonzi mengi, kwani hicho kinyweo cha dada yako Samaria ni kinyweo chenye mastusho na ukiwa. Utakinywa, mpaka ukimalize kwa kufyonza, kisha sharti uvilambe navyo vigae vyake na kuyakwaruza maziwa yako, kwani mimi nimeyasema; ndivyo asemavyo Bwana Mungu. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa umenisahau, ukanitupa mgongoni kwako, basi, wewe nawe jitwike uzinzi wako na ugoni wako! Bwana akaniambia: Mwana wa mtu, hutamhukumu Ohola naye Oholiba? Waumbulie machukizo yao! Kwani wamevunja unyumba, nazo damu zimo mikononi mwao. Unyumba wameuvunja wakiyatamani magogo yao ya kutambikia nao wana wao, walionizalia mimi, wamewapitisha motoni, wayawie vipaji vya tambiko vya kula. Tena wamenifanyizia nayo hayo: Siku ileile wamepatia Patakatifu pangu uchafu, wakazitangua siku zangu za mapumziko. Walipowachinja wana wao kuwa ng'ombe za tambiko za yale magogo yao, siku ileile wakapaingia Patakatifu pangu, wapatie uchafu. Tazama, hivyo ndivyo, walivyofanya Nyumbani mwangu. Tena wametuma hata kwa waume walioko mbali, waje wakitoka kwao; nao hapo, mjumbe alipotumwa kuwaita, ndipo, walipokuja papo hapo. Kwa ajili yao ukaenda koga, ukajitia wanja machoni, ukajipamba na kuvaa mapambo ya urembo. Kisha ukajikalisha katika kitanda kizuri mno, mbele yako pakawa na meza iliyotandikwa, juu yake ukayaweka mavukizo yangu na mafuta yangu. Wakatulia hapo pako na kupiga makelele kama ya watu wengi, wakatuma kuita watu wakaao kwenye watu wengi, wakaletwa wanywaji waliotoka nyikani, wakawapa vikuku vya kuvaa mikononi pao na vilemba vyenye utukufu kuvaa vichwani pao. Nikasema: Hivyo, alivyochakaa kwa kuvunja unyumba, hata sasa ataufanya ugoni wake. Naye akaufanya. Watu wakaja nyumbani mwake, kama wanavyoingia mwake mwanamke mgoni; hivyo ndivyo walivyoingia mwake Ohola namo mwake Oholiba, kwa kuwa wanawake wenye uzinzi. Lakini waume waongofu watawakatia shauri liwe shauri lipasalo wazinzi, tena liwe shauri lipasalo waliomwaga damu kwani ndio wake wazinzi, nazo damu zimo mikononi mwao, Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wakusanyie mkutano mkubwa uwatoe, watupwe huko na huko, kisha wanyang'anywe mali zao! Kisha watu wa huo mkutano wawapige mawe, halafu wawakatekatekwa panga zao! Nao wana wao wa kiume na wa kike wawaue! Tena nyumba zao waziteketeze kwa moto. Hivyo ndivyo, nitakavyoukomesha uzinzi, uishe katika nchi hii, wanawake wote waonyeke, wasifanye uzinzi kama wao. Hivyo ndivyo, watakavyowatika uzinzi wenu, nayo makosa ya kuyatambikia yale magogo yenu mtatwikwa; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia katika mwaka wa 9 katika mwezi wa kumi siku yake ya kumi kwamba: Mwana wa mtu, jiandikie jina lake siku hii siku hiihii ya leo! Kwani mfalme wa Babeli ameufikia Yerusalemu siku hii ya leo. Nao mlango huu mkatavu uutungie fumbo ukiwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Iteleke nyungu! Ndiyo, iteleke! Kisha itie nayo maji! Tena vikusanye vipande vyake vya kutia ndani, vyote viwe vipande vizuri tu vya paja na vya mkono, ijaze mifupa iliyochaguliwa! Chukua kondoo tu waliochaguliwa kwa uzuri! Tena chini yake hiyo nyungu patupie mifupa, iwe chungu! Zitokose kabisa nyama, nayo mifupa iliyomo sharti ichemke sana. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Yatakupata, wewe mji wenye hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Yatakupata, wewe mji wenye damu, u nyungu yenye kutu, nayo kutu yake inakataa kuondoka kwake! Zitoe zile nyama kipande kwa kipande, msizipigie kura! Kwani damu zilizomwagwa mwake zimo bado, ni hapohapo penye mwamba ulio wazi, alipozimiminia, hakuzimwaga penye mchanga, zikafunikwa kwa mavumbi. Kusudi ziyainue makali yangu yenye moto ya kulipiza lipizi, kwa hiyo nimeacha, azimiminie hizo damu penye mwamba ulio wai, zisifunikwe. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Yatakupata, wewe mji wenye damu, nami nitaupangia chungu kubwa la kuni. Lete kuni nyingi, uwashe moto! Zitokose nyama kabisa na kuziunga kwa viungo! Mifupa na iungue! Nyungu ikiwa tupu, iweke penye makaa yake ya moto, chuma chake kipate moto kabisa, mpaka kiungue, taka zake zilizomo ziyeyuke, kutu nayo iondoke kabisa. Lakini ni kujisumbua bure, kutu haitoki kwake kwa kuwa kutu ni nyingi, namo motoni hiyo kutu yake inakaa. Ni kwa ajili ya uchafu wako wa uzinzi; kwa kuwa nilitaka kukutakasa, ukakataa kutakata uchafu wako ukikutoka, kwa hiyo hutatakata tena, mpaka niyatimize kwako makali yangu yenye moto. Mimi Bwana nimeyasema, kwa hiyo yatakuja nitakayoyafanya. Sitachoka, wala sitakuonea uchungu, nikuhurumie; kwa hivyo, njia zako zilivyo, tena kwa hivyo, nayo matendo yako yalivyo, watakuhukumu; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, tazama, ayapendezaye macho yako nitamchukua kwako kwa mara moja nikimpiga; nawe usimwombolezee, wala usimlilie, machozi yasikutoke machoni! Piga kite usiposikiwa; lakini aliyekufa usimfanyizie matanga! jifunge kilemba chako, kavae viatu miguuni pako! Lakini usiufunike udevu wa midomoni, wala usile chakula, watu watakachokuletea! Asubuhi nilikuwa nikisema na watu, tena jioni mke wangu akafa, kesho yake asubuhi nikafanya nilivyoagizwa. Watu wakaniuliza: Mbona hutuelezi yatakayokuwa kwetu, wewe ukifanya hivyo? Nikawaambia: Neno la Bwana limenijia la kwamba: Uambie mlango wa Isiraeli: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikipapatia uchafu Patakatifu pangu palipo majivuno yenu makuu na tamaa ya macho yenu na upendeleo wa roho zenu. Nao wana wenu wa kiume na wa kike, mliowaacha, wataangushwa kwa panga. Ndipo, mtakapofanya, mimi nilivyofanya: Hamtazifunika ndevu za midomoni, wala hamtakula chakula, mtakacholetewa na watu. Navyo vilemba vyenu vitakuwa vichwani penu, navyo viatu miguuni penu; hamtaomboleza, wala hamtalia machozi, ila kwa manza zetu, mlizozikora, mtayeyuka, tena mtapigiana kite kila mtu na ndugu yake. Naye Ezekieli atawawia kielekezo, nanyi myafanye yote, aliyoyafanya yeye, yatakapotimia. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu. Nawe mwana wa mtu, isiwe hivyo? Siku, nitakapoyachukua kwao yaliyowapa nguvu, yaliyokuwa furaha yao kwa kuwapa utukufu, macho yaliyoyatamani, yaliyowashika mioyo yao wana wao wa kiume na wa kike, siku ile atakuja kwako mtu aliyekimbia, ayasimulie masikioni pako. Siku ile kinywa chako kitafumbuliwa papo hapo, yule mtoro atakapofika kwako, useme, usinyamaze tena; ndipo, utakapowawia kielekezo, nao watajua, ya kuwa mimi ni Bwana. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, waelekezee wana wa Amoni uso wako, uwafumbulie yatakayokuwa! Waambie wana wa Amoni: Lisikieni neno la Bwana Mungu! Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa ulipazomea Patakatifu pangu, palipotiwa uchafu, kwa kuwa uliizomea nayo nchi ya Isiraeli, ilipoangamizwa, ukawagutia nao walio mlango wa Yuda, walipotekwa na kuhamishwa, kwa hiyo utaniona, nikikutia mikononi mwao watakao maawioni kwa jua, waichukue nchi yako, iwe yao, wayapige mahema yao kwako, waitumie nchi yako kuwa makao yao; hao ndio watakaoyala matunda yako, tena ndio watakaoyanywa maziwa yako. Nao mji wa Raba nitautoa kuwa malisho ya ngamia, navyo vijiji vya wana wa Amoni vitakuwa matulio ya makundi ya mbuzi na kondoo. Ndipo mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa ulipiga makofi pamoja na kupiga shindo kwa miguu yako, ukafurahi kwa moyo wako wote ulio wenye mabezo kwa ajili ya nchi ya Isiraeli, kwa hiyo utaniona, nikikukunjulia mkono wangu, nikutolee mataifa mengine, wakunyang'anye, kisha nitakuangamiza kwenye makabila ya watu, nikupoteze na kukutowesha katika nchi hizi. Ndipo, utakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa Wamoabu na Waseiri husema: Tazameni, mlango wa Yuda unafanyiziwa kama mataifa yote, kwa hiyo mtaniona, nikiufunua ubavu wake Moabu kuanzia kwenye miji, kwenye ile miji yake iliyoko mipakani, iliyokuwa urembo wa nchi, kama Beti-Yesimoti na Baali-Meoni na Kiriataimu. Nchi yao nitaitoa nayo yao wana wa Amoni, niwape watokao maawioni kwa jua, iwe yao, kusudi wana wa Amoni wasikumbukwe tena kwenye mataifa. Wamoabu nao nitawahukumu; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa Waedomu walijilipiza kwao wa mlango wa Yuda na kuwatoza malipizi, wamekora manza papo hapo, walipojilipiza kwao. Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Nitaikunjulia nchi ya Waedomu mkono wangu niangamize kwake watu na nyama, niigeuze kuwa mabomoko tu, kuanzia Temani mpaka Dedani watu watauawa kwa panga. Nami nitawatia mikononi mwao walio ukoo wangu wa Isiraeli, wawatoze malipizi, niyatakayo, wakiwafanyizia Waedomu mambo, machafuko yangu makali yenye moto yanayoyataka, wapate kujua, ya kuwa lipizi ni langu mimi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa Wafilisti waliendelea kujilipiza, wakijilipiza na kutoza malipizi kwa mioyo yenye mabezo, wakayazidisha mabaya yao kwa kushika machukio ya kale na kale, kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Mtaniona, nikiwakunjulia Wafilisti mkono wangu, niwaangamize hao Wakreta na kuyapoteza masao yao yaliyoko pwani kwenye bahari. Nami nitawatoza malipizi makubwa na kuwapiga kwa makali yenye moto. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapowatoza malipizi yangu. Ikawa katika mwaka wa 11 siku ya kwanza ya mwezi, ndipo, neno la Bwana liliponijia la kwamba: Mwana wa mtu, Watiro waliuzomea Yerusalemu kwamba: Aha! umevunjika uliokuwa umeingiwa na makabila ya watu! Sasa watageuka, waje kwangu! Bado kidogo nitafurikiwa, kwa kuwa umebomoka! Kwa sababu hii Bwana Mungu anasema hivi: Utaniona, nikikujia, wewe Tiro! Nitaleta mataifa mengi, wakupige, kama bahari inavyoleta mawimbi kwa mawimbi. Wataziangusha kuta za boma lake Tiro na kuibomoa minara yake nami nitauparapara mchanga wake, upatoke, mpaka nipageuze mahali pake kuwa mwamba mtupu. Hivyo patakuwa tu pa kuanikia nyavu katikati ya bahari, kwani mimi nimeyasema; nayo mataifa watapanyang'anyiana; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Navyo vijiji vyake ulivyovijenga mrimani, watu wao watauawa kwa panga; ndipo watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikimleta Nebukadiresari, mfalme wa Babeli, aliye mfalme wa wafalme, aujie mji wa Tiro na kutoka kaskazini na kuleta farasi na magari ya watu wapandao farasi na vikosi vingi vya makabila ya watu. Waliomo katika vijiji vyako vya mrimani atawaua kwa panga; kisha atakujengea minara ya vita, tena atakuzungushia ukingo wa mchanga na kukujengea hapohapo vibanda kuwa ngao zao. Kisha atazipiga kuta za boma lako kwa vyombo vyake vya kubomolea, nayo minara yako ataivunja kwa vyuma vyake. Kwa kuwa na farasi wengi mavumbi yao yatakufunika, kwa mashindo ya wapanda farasi na za magurudumu na za magari kuta zako zitatetemeka, atakapoingia katika malango yako, kama watu wanavyoingia katika mji uliovunjwa kwa nguvu. Kwa kwato za farasi wake atazipondaponda barabara zako zote za mjini, walio ukoo wako atawaua kwa panga, nazo nguvu za vinyago vyako zitaangushwa chini. Vilimbiko vyako watavinyang'anya, nazo mali zako za kuchuuzia wataziteka, kuta zako za boma watazibomoa, majumba yako, uliyoyatamani kwa uzuri wao, watayavunja, kisha watayatupa baharini mawe yako na miti yako na mavumbi yako. Ndipo, nitakapozikomesha shangwe za nyimbo zako, zisisikiwe tena sauti za mazeze yako. Hivyo nitakugeuza kuwa mwamba mtupu, uwe mahali pa kuanikia nyavu, hutajengwa tena, kwani mimi Bwana nimeyasema; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema kwa ajili ya Tiro: Je? Kwa uvumi wa anguko lako, kwa mauguzi yao walioumizwa na kuuawa kabisa kwa panga mjini mwako nchi za pwani zisitikisike? Wafalme wote wa nchi zilizoko baharini watashuka katika viti vyao vya kifalme wakiziondoa kanzu zao za urembo na kuzivua nazo nguo zao za rangi, kisha watajivika mastuko na kukaa chini, wakistuka mara kwa mara kwa kupigwa na bumbuazi kwa ajili yako. Kisha watakutungia ombolezo la kukulilia kwamba: kumbe umeangamia uliokaa baharini, uliokuwa mji wa kusifiwa tu kwa kukaa na nguvu zake baharini, huo wenyewe na watu wake waliokuwamo waliowatisha wote waliokaa pwani kwao! Siku hiyo, utakapoangushwa, nchi zilizoko baharini zitakuwa zimestuka, navyo visiwa vilivyomo baharini vitakuwa vimetishika sana kwa kutoweka kwako. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nitakapokutoa kuwa mji uliobomolewa, kuwa kama miji mingine isiyokaa watu, nitakapokupandishia mawimbi ya bahari, maji yao mengi yakufunike, ndipo, nitakapokusukuma, ushuke kwao walioshuka shimoni, kwao watu wa kale, ndipo nitakapokukalisha kuzimuni chini ya nchi kwenye mabomoko ya kale kwao washukao shimoni, kusudi watu wasikae mwako tena. Lakini nchi yao walio wazima nitaipitia urembo mwingine. Nitakapokutisha, utakuwa umetoweka, usioneke tena kale na kale, ijapo watu wakutafute; ndivyo asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Wewe mwana wa mtu, utungie mji wa Tiro ombolezo! Uambie Tiro: Wewe ulikaa paingiapo bahari, ukachuuza katika nchi nyingi za baharini; hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wewe Tiro ulisema: Mimi nimetimiza uzuri wote. Kweli mipaka yako imo baharini ndani, nao waliokujenga walikutengeneza kuwa chombo chenye uzuri wote. Walikujenga pande zote mbili kwa mbao za mivinje ya Seniri, wakachukua mwangati huko Libanoni wa kukutengenezea mlingoti. Mivule ya Basani waliitumia ya kukufanyizia makasia, vyumba vyako walivifanya kwa mbao za misagawi zilizopangiliwa kwa meno ya tembo, zilizotoka visiwani kwa Wakiti. Nguo za rangi zilizotoka Misri zilikuwa tanga lako zikawa hata bendera yako. Nguo za kifalme nyeusi na nyekundu zilizotokavisiwa vya Elisa zilikuwa chandalua chako cha kujifunika juu. Waliokaa Sidoni na Arwadi walikuwa mabaharia wako, nao werevu wa kweli wa kwako, Tiro, ndio waliokuwa waelekeza chombo. Wazee wa Gebali na mafundi wake walikuwa kwako wa kuziziba nyufa zako. Merikebu zote za baharini zikafika kwako na mabaharia wao, wakauziana na wewe. Wapersia na Waludi na Waputi walikuwamo katika vikosi vyako vya askari wa kukupigia vita vyako; walipotundika ngao na kofia kwako waliuongea utukufu wako. Wana wa Arwadi na askari wako walizunguka penye kuta zako za boma, tena Wagamadi walikuwa katika minara yako; walipozitundika ngao zao po pote katika kuta zako, waliutimiza uzuri wako. Watarsisi wakaja kuchuuza kwako kwa ajili ya wingi wa vitu vya kwako, wakazinunua bidhaa zako kwa fedha na kwa vyuma na kwa bati na kwa risasi. Wagriki na Watubali na Wameseki walikuwa wachuuzi wako, wakatoa watumwa na vyombo vya shaba, wapate vitu vya kwako. Walio wa mlango wa Togarma walitoa farasi na farasi wa vita na nyumbu, wapate bidhaa zako. Wana wa Dedani walikuwa wachuuzi wako, watu wa nchi nyingi za baharini wakaja kuchuuza mikononi mwako: walikuletea meno ya tembo na mipingo kuwa malipo yao. Washami nao wakaja kuchuuza kwako kwa ajili ya wingi wa kazi zako, wakazinunua bidhaa zako kwa vito vyekundu na kwa nguo za kifalme na kwa nguo za rangi na kwa bafta nzuri na kwa marijani na kwa vijiwe vya yaspi. Wayuda nao wa nchi ya Isiraeli walikuwa wachuuzi wako, wakanunua vitu vya kwako kwa ngano za Miniti na kwa vikate vitamu na kwa asali na kwa mafuta na kwa uvumba. Wadamasko wakaja kuchuuza kwako kwa ajili ya wingi wa kazi zako na kwa ajili ya wingi wa mali, wakaleta mvinyo za Helboni na manyoya meupe sana ya kondoo. Wawedani na Wayawani walijipatia bidhaa zako na kuleta toka Uzali vyuma vilivyofuliwa vema, hata dalasini na vichiri vilikuwa malipo yao ya kukulipa. Wadedani walikuwa wachuuzi wako, wakanunua vyako kwa nguo nzuri za kuweka chini ya matandiko. Waarabu na wakuu wote wa Kedari nao wakaja kuchuuza mikononi mwako, wakanunua kwako kwa wana kondoo na kwa madume ya kondoo na kwa mbuzi. Wachuuzi wa Saba na wa Raama nao walikuwa wachuuzi wako, wakazinunua bidhaa zako kwa manukato mazuri mno kupita yote mengine na kwa vito vya namna zote vyenye kiasi kikubwa na kwa dhahabu. Waharani na Wakane na Waedeni, nao wachuuzi wa Saba na Waasuri na Wakilmadi walikuwa wachuuzi wako. Hao walifanya biashara na wewe wakiuza nguo za urembo kama mablanketi makubwa ya kifalme yenye rangi nzuri na mazulia yenye machorochoro yaliyofungwa vema kwa kamba katika sanduku za miangati, wakanunua vitu vilivyouzwa kwako. Merikebu za Tarsisi zilikuwa kama wapangazi wako wa kupeleka vitu vya kwako, ukafurikiwa, ukatukuka sana huko ndani baharini. Wavutao makasia wakikupeleka kwenye vilindi vya maji, lakini upepo utokao maawioni kwa jua utakuvunja baharini kati. Ndipo, mali zako na bidhaa zako na vitu vya kwako na mabaharia wako na waelekeza chombo nao wazibao nyufa zako nao wachuuzi waliovichuuzia vya kwako nao wote, ulio nao wa kukupigia vita vyako, pamoja na mkutano wote wa watu wako waliomo mwako watakapoanguka kule baharini kati; itakuwa siku ile, utakapoangamizwa. Kwa sauti za makelele ya waelekeza vyombo vyako vitatetemeka viunga vyako. Ndipo, wote wavutao makasia watakaposhuka na kutoka merikebuni mwao mabaharia nao wote waelekezao vyombo baharini wasimame pwani, wakupalizie sauti zao na kukulilia kwa uchungu; watajitupia mavumbi vichwani pao na kujigaagaza majivuni. Watajikata nywele kwa ajili yako, vichwa viwe vyenye vipara, kisha watajifunga magunia, wakulilie kwa uchungu wa roho zao na kukuombolezea kwa kuliwa na uchungu. Watakapokulilia watakutungia ombolezo, wakuombolezee kwamba: Pako mahali gani panaponyamaza kimya kama Tiro ulioko baharini kati? Bidhaa zako zilipotoka baharini ulishibisha makabila mengi ya watu, kwa wingi wa mali zako na wa vitu vya kwako uliwapatia wafalme wa nchi mali nyingi. Lakini sasa umevunjwa, utoweke baharini kwa kutoswa vilindini penye maji mengi, navyo vitu vya kwako vya kuuza nao mkutano wa watu wako waliokuwamo mwako wamezama. Kwa hiyo wote wakaao kwenye bahari wanakustukia wafalme wao wakapigwa na bumbuazi, nazo nyuso zao zikatetemeka. Wachuuzi walioko kwenye makabila ya watu hukuzomea, kwa kuwa umegunduliwa na maangamizo, wala hutakuwapo tena kale na kale. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, mwambie mfalme wa Tiro: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Moyo wako umejikuza kwamba: Mungu ni mimi, tena ninakaa pake Mungu baharini katikati! Kumbe nawe u mtu, hu Mungu, nawe moyo wako ukajiwazia kuwa kama moyo wa Mungu! Je? Wewe u mwerevu wa kweli kuliko Danieli, lisifichike jambo lo lote, usipolipambazua? Kwa werevu wako wa kweli na kwa utambuzi wako ulijipatia mali, ukalimbika dhahabu na fedha katika maweko yako. Kwa kuwa mwenye werevu mwingi ulio wa kweli ukaziongeza sana mali zako kwa biashara zako, ulizozifanya; kwa hizo mali zako moyo wako ukajikuza. Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Kwa kuwa moyo wako unajiwazia kuwa kama moyo wa Mungu, kwa sababu hiyo utaniona, nikikupelekea wageni, ndio mataifa yenye ukali kupita wengine. Nao watazichomoa panga zao kupigana na uzuri wa werevu wako wa kweli, wauchafue uangafu wako. Watakusukuma, ushuke shimoni, nawe utakufa baharini katikati, kama waliopigwa na panga wanavyokufa. Je? Usoni pa mwuaji utasema tena: Mungu ni mimi? Nawe u mtu, hu Mungu, tena utakuwa mkononi mwake akupigaye kwa upanga. Utakufa mikononi mwa wageni, kama wanavyokufa wasiotahiriwa, kwani mimi nimeyasema; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, mtungie mfalme wa Tiro ombolezo! Mwambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wewe ulikuwa kielelezo cha ulinganifu, tena mwenye werevu wa kweli mwingi na mwenye kuutimiza uzuri. Ukawa Edeni katika bustani ya Mungu, ukalipamba vazi lako kwa vito vya kila namna: sardio na topazio na yaspi na krisolito na oniki na berilo na safiro na ametisto na sumarato na dhahabu; siku hiyo ulipoumbwa, kazi za patu zako na filimbi zako zilikuwa zimetengenezwa, zikuwie tayari. Ukawa kama Kerubi aliyepakwa mafuta kuwa mlinzi, nikakuweka juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, ukawako ukitembea katika mawe yenye moto katikati. Ukawa pasipo kosa lo lote katika njia zako tangu siku ile, ulipoumbwa, mpaka upotovu ulipooneka kwako. Lakini kwa uchuuzi wako mwingi ukajaa makorofi ndani yako, ukakosa, nami nikakukimbiza kwenye mlima wa Mungu, kwa kuwa ulijipatia uchafu, nikakutowesha uliyekuwa kama Kerubi alindaye, uondoke katika yale mawe yenye moto. Moyo wako ulijikuza kwa ajili ya uzuri wako, ukauharibu werevu wako wa kweli kwa ajili ya uangafu wako; ndipo, nilipokubwaga chini, nikakutoa machoni pao wafalme, wakutumbulie macho. Kwa manza zako nyingi ulizozikora, tena kwa kupotoa uchuuzi wako, ulipatia Patakatifu pako uchafu; kwa hiyo nikatoa moto mwako katikati, ukakuteketeza, nikakutoa kuwa mavumbi ya nchi machoni pao wote waliokutazama. Wote waliokujua katika makabila ya watu hukustukia, kwa kuwa umegunduliwa na maangamizo, nawe hutakuwapo tena kale na kale. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, uuelekezee Sidoni uso wako na kuufumbulia yatakayokuwa! Sema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikikujia, Sidoni, nijitokeze katikati yako kuwa mtukufu. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapouhukumu, nijulike mwake, ya kuwa ni mtakatifu. Nitatuma kwake magonjwa mabaya na damu barabarani mwake, waangushwe mwake chini po pote waliopigwa kwa panga; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Mlango wa Isiraeli hautaona tena miiba ya kuwachoma wala machomo ya kuwaumiza kwao wote wanaokaa na kuwazunguka waliowabeza; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nitakapowakusanya walio ukoo wa Isiraeli na kuwatoa kwenye makabila yote, walikotawanyikia, ndipo, nitakapoutokeza kwao utakatifu wangu, wao wa mataifa wauone; nao watakaa katika nchi yao, niliyompa mtumishi wangu Yakobo. Nao watakaa huko kwa kutulia, wajenge nyumba, wapande mizabibu; watakaa kwa kutulia, kwa kuwa nitawakatia mashauri kwao wote wanaokaa na kuwazunguka waliowabeza. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu wao. Katika mwaka wa 10 katika mwezi wa kumi siku yake ya kumi na mbili neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, mwelekezee Farao, mfalme wa Misri, uso wako na kumfumbulia yote yatakayomjia yeye nayo nchi yake yote nzima ya Misri! Sema ukimwambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikikujia, wewe Farao, mfalme wa Misri, uliye mamba mkubwa aoteaye katika majito yake katikati na kusema: Ni langu hili jito langu, nami nimelifanyizia kuwa langu! Nitakutia ndoana kubwa katika taya zako, kisha nitawagandamanisha samaki wa majito yako magambani pako, nikupandishe na kukutoa ndani ya majito yako pamoja na samaki wote waliomo majitoni mwako, wakigandamana na magamba yako. Kisha nitakubwaga nyikani wewe pamoja na samaki wote waliokuwamo majitoni mwako, hutaokotwa wala hutakusanywa, ila nitakutoa, nyama wa porini na ndege wa angani wakule. Ndipo, wote wakaao Misri watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, kwa kuwa walikuwa kwao wa mlango wa Isiraeli kama mwanzi wa kujiegemezea. Lakini walipokushika mikononi mwao, ukakunjika, ukawapasua mabega yao yote; tena walipojiegemeza kwako, ukavunjika na kuvilemaza viuno vyao vyote. Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Utaniona, nikikupelekea panga, niangamize kwako watu na nyama. Ndipo, nchi ya Misri itakapokuwa peke yake kwa kuharibiwa, ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, kwa kuwa alisema: Jito ni langu, mimi ndiye aliyelifanya. Kwa hiyo utaniona, nikikujia wewe, hata majito yako, niitoe nchi ya Misri, iharibiwe kabisa, mpaka iwe peke yake tu kuanzia Migidoli kufikisha Siwene hata mipaka ya Nubi. Hautapita kwake mguu wa mtu, wala mguu wa nyama hautapita kwake, wala hawatakaa watu miaka 40. Nitaitoa nchi ya Misri kuwa peke yake katikati ya nchi nyingine zilizo peke yao nazo, nayo miji yake itakuwa peke yao katikati ya miji mingine iliyo mabomoko tu, itakuwa hivyo miaka 40. Nao Wamisri nitawatawanya kwenye mataifa mengine na kuwatupatupa katika nchi zao. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Miaka 40 itakapokwisha, nitawakusanya Wamisri na kuwatoa kwenye makabila ya watu, walikotawanyikia. Ndipo, nitakapoyafungua mafungo yao Wamisri, niwarudishe katika nchi ya Patirosi, ndiyo nchi, waliyozaliwa; ndiko, watakakokuwa ufalme ukaao chini tu. Katika nchi za kifalme nyingine itakaa chini tu, haitaweza kuyainukia mataifa tena, kwani nitawapunguza, wawe wachache tu, wasiyatawale mataifa. Wala hawatakuwa tena egemeo lao mlango wa Isiraeli la kunikumbusha manza, walizozikora walipowageukia kuwafuata. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu. Ikawa katika mwaka wa 27 siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, ndipo, neno la Bwana liliponijia la kwamba: Mwana wa mtu, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, amevitumikisha vikosi vyake utumishi mkubwa huko Tiro, mpaka vichwa vyote vikapata vipara, nayo mabega yote yakachubuka, lakini hakuna walichokipata huko Tiro, wala yeye wala vikosi vyake, kwa huo utumishi wao, waliomtumikia kule. Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Mtaniona, nikimpa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, nchi ya Misri, azichukue mali zao na kuyateka mateka yao na kuyapokonya mapokonyo yao; hayo yatakuwa mshahara wa vikosi vyake. Kwa kumlipa kazi zake, alizozitumikia huko, nitampa nchi ya Misri, kwa kuwa amenifanyizia kazi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Siku ile nitakuza pembe kwao wa mlango wa Isiraeli, nami nitakupa kukifunua kinywa chako katikati yao; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, fumbua yatakayokuwa, ukisema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Pigeni vilio kwamba: Ni siku gani hii? Kwani siku iko karibu, kweli siku ya Bwana iko karibu! ni siku yenye mawingu, itakuwa wakati wa wamizimu. Panga zitaingia Misri, nayo nchi ya Nubi itatetemeka, watu waliopigwa kwa panga wakianguka huko Misri, wengine wakizichukua mali zao, tena wakiibomoa misingi yao. Wanubi na Waputi na Waludi nao wote waliochanganyika nao na Wakubu na wenyeji wa nchi, waliofanya maagano nao, wote pia watauawa kwa panga. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nao walioiegemea nchi ya Misri wataangushwa, majivuno ya nguvu zake yakinyenyekezwa; kuanzia Migidoli kufikisha Siwene watauawa kwao kwa panga; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Nchi zao zitakuwa peke yao katikati ya nchi nyingine zilizo peke yao nazo, nayo miji yao itakuwa vivyo hivyo katikati ya miji iliyo mabomoko tu. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana; nitakapowasha moto katika Misri, nao wasaidiaji wake wote watavunjwa. Siku ile watatoka kwangu wajumbe kwenda katika merikebu kuwastusha nao Wanubi wakaao na kutulia; ndipo, watakapotetemeka, ile siku ya Misri itakapokuja, kwani wataiona, inavyokuja. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nitawakomesha wale watu wengi wa Misri kwa mkono wa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli. Yeye na watu wake, alio nao, ni wakali kuliko mataifa mengine; watapelekwa kuiangamiza hiyo nchi, watazichomoa panga zao kuwapiga Wamisri, waijaze hiyo nchi watu walioumizwa na panga. Nayo majito yake nitayakausha, nayo nchi hiyo nitaiuza mikononi mwa watu wabaya, niiangamize kwa mikono ya wageni pamoja nayo yote yaliyomo. Mimi Bwana nimeyasema. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nitayapoteza magogo ya kutambikia mle Nofu, hata vinyago nitavikomesha, pasiwe tena mkuu atokaye katika nchi ya Misri, tena nitaitisha nchi ya Misri. Patirosi nitaigeuza kuwa mapori tu, mle Soani nitawasha moto, namo No nitawahukumu waliomo. Mji wa Sini ulio boma lake Misri nitaumwagia makali yangu yenye moto, nao watu wengi waliomo No nitawaangamiza. Nitawasha moto katika Misri: Sini utaona machungu makuu, No utavunjwa kwa kubomolewa, Nofu utapata wanaousonga mchana. Vijana wa Oni na wa Pi-Beseti watauawa kwa panga, watu wao wengine watatekwa na kuhamishwa. Namo Tehafunesi mchana utageuka kuwa giza, nitakapozivunja mle bakora za kifalme za Misri; namo ndimo, nitakamoyakomesha majivuno ya nguvu zao; mji wenyewe wingu litaufunika, navyo vijiji vyake vya shambani vitatekwa na kuhamishwa. Hivyo ndivyo, nitakavyokata mashauri huko Misri; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Ikawa katika mwaka wa 11 siku ya saba ya mwezi wa kwanza, ndipo, neno la Bwana liliponijia la kwamba: Mwana wa mtu, mkono wa Farao, mfalme wa Misri, nimeuvunja, lakini tazama, haukufungwa, upate kupona, hawakuutakia kitambaa tu, kwamba waufunge, wautie nguvu tena, upate kushika upanga. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikimjia Farao, mfalme wa Misri, nitaivunja mikono yake, ule ulio na nguvu bado nao ule uliokwisha kuvunjika, niuangushe upanga chini uliomo mkononi mwake. Nao Wamisri nitawatawanya kwenye mataifa mengine na kuwatupatupa katika hizo nchi. Lakini mikono ya mfalme wa Babeli nitaitia nguvu, nao upanga wangu nitampa mkononi mwake, niivunje mikono ya Farao, ampigie yeye kite kama mtu mwenye vidonda. Mikono ya mfalme wa Babeli nitaitia nguvu, lakini mikono ya Farao itaanguka; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapompa mfalme wa Babeli upanga wangu mkononi mwake, aichomolee nchi ya Misri. Nao Wamisri nitawatawanya kwenye mataifa mengine na kuwatupatupa katika hizo nchi. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Ikawa katika mwaka wa 11 siku ya kwanza ya mwezi wa tatu, ndipo neno la Bwana liliponijia la kwamba: Mwana wa mtu, mwambie Farao, mfalme wa Misri, nao watu wake walio wengi: kwa ukuu wako unafanana na nani? Tazama, Mwasuri alikuwa mwangati wa Libanoni ulio mzuri kwa matawi yake yaliyo yenye majani mengi yenye kivuli, tena ni mrefu kwa kimo chake, kilele chake huyapita majani mengine ya miti iliyoko. Maji ndiyo yaliyoukuza hivyo, vilindi vya chini ndivyo vilivyouendesha juu, mito yao ikapitia po pote ulipopandwa, kisha vikavipeleka vijitojito vyao penye miti yote ya shambani. Kwa hiyo ulikua kuwa mrefu kwa kimo chake kuliko miti yote ya kondeni, matawi yake yakawa mengi, nayo machipuko yake yakawa marefu, ukiweza kuyachipuza vema kwa hayo maji mengi. Ndege wote wa angani walijenga matundu yao katika matawi yake, hapo chini ya machipuko yake wakazaa nyama wo wote wa porini, napo kivulini pake wakakaa mataifa mengi na mengi. Hivyo ulikuwa mzuri kwa ukubwa wake na kwa urefu wa matawi yake, kwani mizizi yake iko kwenye maji mengi. Katika bustani ya Mungu haukuwako mwangati ulioupita, wala mivinje haikufanana nao kwa matawi yao, wala migude haikuwa yenye machipuko kama huo; miti yote iliyoko bustanini kwake Mungu haikufanana nao kwa uzuri wake. Niliutengeneza kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake, kwa hiyo miti iliyoko Edeni bustanini kwake Mungu iliuonea wivu. Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Kwa kuwa ulikuwa mrefu kwa kimo chake, kilele chake kikayapita majani ya miti iliyoko, ukajiwazia moyoni mwake kuwa mkuu kwa urefu wake. Lakini nitamtia mikononi mwake aliye peke yake mkuu wa mataifa, aufanyizie ayatakayo; kwa uovu wake nimekwisha kuutupa. Ndipo, wageni walio wakali kuliko mataifa mengine walipoukata, wakaubwaga, matawi yake yaanguke milimani na mabondeni po pote, nayo machipuko yake yakavunjika, yakawa katika makorongo yote ya nchi, nayo makabila yote ya nchi yakaondoka kivulini pake, wakauacha tu. Juu ya gogo lake lililoanguka watakaa ndege wote wa angani, nako kwenye machipuko yake watakuwako nyama wote wa porini. Itakuwa hivyo, kusudi miti yote iliyoko kwenye maji isijikuze, wala isipeleke vilele vyao juu kabisa kupita miti mingine yenye majani mengi, wala ile yenye nguvu isisimame kwa urefu wao na kuishinda yote mingine inyweshwayo, kwani yote imewekewa kufa, ifike mahali palipo chini ya nchi kwenye watu walioshuka shimoni. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Siku ile, uliposhuka kuzimuni, naliviombolezesha vilindi vya maji vilivyoko ndani ya nchi nikivifunika kwa ajili yake huo, tena nikiizuia mito yao, yale maji mengi yakomeshwe, nayo milima ya Libanoni naliivika mavazi ya matanga, nayo miti yote ya kondeni ikazimia. Kwa uvumi wa kuanguka kwake nikayatetemesha mataifa, nilipoushusha kuzimuni pamoja nao washukao shimoni; ndipo, miti yote ya Edeni ilipotulizana pale mahali palipo chini ya nchi, ni ile miti ya Libanoni iliyochaguliwa kwa uzuri, ile yote iliyonyweshwa maji. Hii nayo ilishuka pamoja nao kuzimuni kwao waliouawa kwa panga, ndio waliokuwa mkono wake walipokaa kivulini pake katikati ya mataifa. Kwa hiyo umefanana na nani kwa utukufu na kwa ukuu kwenye miti ya Edeni? Pamoja na miti hii ya Edeni nawe utashushwa pale mahali palipo chini ya nchi, ulale kwao wasiotahiriwa pamoja nao waliouawa kwa panga. Huo ndio Farao na watu wake wote walio wengi. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Ikawa katika mwaka wa 12 siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na mbili, ndipo, neno la Bwana liliponijia la kwamba: Mwana wa mtu, mtungie Farao, mfalme wa Misri, ombolezo la kwamba: Ulifananishwa na mwana wa simba alioko kwenye mataifa, nawe ulikuwa kama mamba aliomo kwenye maji mengi, mara kwa mara ulitokea kwa nguvu katika mito yako, ukachafua maji kwa miguu yako na kuivurugavuruga mito yao. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nitautanda wavu wangu juu yako kwenye mkutano wa makabila mengi ya watu, nao watakupandisha pakavu kwa jarife langu. Kisha nitakuacha hapo penye nchi kavu nikikutupa porini; kisha nitaleta ndege wa angani wote, wakukalie, nao nyama wote wa nchi hiyo nitawashibisha kwako. Hata milimani juu nitazipeleka nyama za mwili wako, nayo mabonde nitayajaza uvundo wa kwako. Nchi nitainywesha mafuriko yako yatokayo kwa damu yako, yafike hata milimani, nayo makorongo yatajazwa hayo yatokayo kwako. Hapo, nitakapokuzima, nitaifunika mbingu, nazo nyota zake nitazitia giza, hata jua nitalifunika kwa wingu, hata mwezi hautaangaza mwanga wake. Mianga yote iangazayo mbinguni nitaitia giza kwa ajili yako, hata nchi yako nitaieneza giza; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Kisha nitasikitisha mioyo ya watu wa makabila mengi, nitakapopeleka habari za kuvunjwa kwako kwa mataifa katika nchi, usizozijua wewe. Hivyo nitastusha makabila mengi kwa ajili yako, nao wafalme wao watapigwa na bumbuazi kwa ajili yako, nitakapouchezesha upanga wangu mbele yao; ndivyo, watakavyoingiwa na woga mara kwa mara, Kila mtu kwa ajili ya roho yake, siku ile, utakapoangushwa. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Upanga wa mfalme wa Babeli utakujia. Kwa panga za wapiga vita wenye nguvu nitawaua watu wako, ingawa wawe wengi, kwani wale wote ndio wakali kuliko mataifa mengine; watayapoteza majivuno ya Wamisri, watu wao walio wengi watakapoangamizwa. Nao nyama wao wote nitawatowesha kwenye yale maji mengi, mguu wa mtu usiyachafue tena, wala nyama asiyachafue kwa kuyavurugavuruga. Ndipo, nitakapoyachuja maji yao, nayo majito yao nitayaendesha kama mafuta yanavyokwenda; ndivyo, asemavyo Bwana. Nitakapoigeuza nchi ya Misri kuwa pori tu, nchi itakapokuwa peke yake tu, yote yaliyoko yakitoweka, nitakapowapiga wote wakaao huko, ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Hili ndilo ombolezo la kuimba kwa kuomboleza; wanawali wa mataifa waliimbe kwa kuiombolezea nchi ya Misri, nao watu wake wengi watawaombolezea hivyo; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Ikawa katika mwaka wa 12 siku ya kumi na tano ya mwezi, ndipo, neno la Bwana liliponijia la kwamba: Mwana wa mtu, walilie hao watu wengi wa Misri, uwashushe pamoja na wanawali wa mataifa wenye utukufu kuwafikisha mahali palipo chini ya nchi kwao washukao shimoni. Unampita nani kwa uzuri? Shuka tu, ulazwe kwao wasiotahiriwa! Wataanguka katikati yao waliouawa kwa panga; panga za kuwaua zimekwisha tolewa; ivuteni hiyo nchi pamoja na watu wake wote walio wengi! Ndipo, wapiga vita wenye nguvu walioko kuzimuni watakapomwambia yeye nao waliomsaidia: Wameshuka kulala hawa wasiotahiriwa waliouawa kwa panga. Wako Waasuri na makundi yao yote ya watu, makaburi yao yanapazunguka pale po pote, wote wamekufa kwa kuumia wakiangushwa kwa panga. Wamepata makaburi yao kuzimuni pembeni, nayo makundi yao ya watu yanayazunguka makaburi yao wenyewe; hao wote wamekufa kwa kuumia wakiangushwa kwa panga; nao ndio waliostusha watu wakubwa katika nchi yao walio hai. Wako Waelamu nao watu wao wengi; wanalizunguka kaburi lake; hao wote wamekufa kwa kuumia wakiangushwa kwa panga, wameshuka pasipo kutahiriwa mahali palipo chini ya nchi; nao ndio waliostusha watu walipokuwa katika nchi yao walio hai, sasa wanashikwa na soni kwao walioshuka shimoni. Katikati yao waliouawa kwa panga wamewapa pa kulala penye watu wao wengi, nayo makaburi yao hawa yanawazunguka wenyewe. Wote ni watu wasiotahiriwa waliouawa kwa panga, kwani walistusha watu walipokuwa katika nchi yao walio hai, lakini sasa wanashikwa na soni kwao walioshuka shimoni, katikati yao waliouawa kwa panga wamepata mahali pao. Wako Wameseki na Watubali nao watu wao wengi, makaburi yao hawa yanawazunguka wenyewe; hawa wote ni watu wasiotahiriwa, walikufa wakiumia kwa panga; kwani walistusha watu walipokuwa katika nchi yao walio hai. Hawatalala pamoja na wapiga vita walioanguka kwao wasiotahiriwa, walioshuka kuzimuni pamoja na vyombo vyao vya vita wakiziweka panga zao chini ya vichwa vyao, lakini maovu, waliyoyafanya, yanaifunika mifupa yao, kwani hao wapiga vita walistusha watu walipokuwa katika nchi yao walio hai. Hivyo wewe nawe utavunjwa katikati yao wasiotahiriwa, ulale nao waliokufa wakiumia kwa panga. Wako Waedomu, wafalme wao na wakuu wao, waliokuwa wenye nguvu za kupiga vita, lakini nao wamepewa mahali pao kwao waliokufa wakiumia kwa panga, walale nao kwao wasiotahiriwa walioshuka shimoni. Wako wakuu wa kaskazini wote pamoja na Wasidoni wote walioshuka kwao waliokufa wakiumia kwa panga; walikuwa wakistusha watu kwa nguvu zao za kupiga vita, lakini soni za kushindwa zikawapata nao, sasa wanalala pasipo kutahiriwa kwao waliokufa wakiumia kwa panga wakishikwa na soni kwao walioshuka shimoni. Farao atakapowaona hao atajituliza kwa ajili ya watu wake waliokuwa wengi. Farao na vikosi vyake vyote watakufa wakiumia kwa panga; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Kwani nalimpa kustusha watu, alipokuwa katika nchi yao walio hai, lakini naye atalazwa katikati yao wasiotahiriwa pamoja nao waliokufa wakiumia kwa panga, yeye Farao nao watu wake walio wengi. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, sema nao walio ukoo wako ukiwaambia: Kama ninailetea nchi panga, watu wa nchi hiyo watamchukua mtu mmoja miongoni mwao, wamweke kuwa mlinzi wao. Atakapoziona panga, zikiijia hiyo nchi, atapiga baragumu, awaonye wale watu. Lakini mtu akiisikiliza tu sauti ya baragumu pasipo kuonyeka, panga zitamkamata, nayo damu yake atatwikwa yeye kichwani. Akiisikia sauti ya baragumu pasipo kuonyeka, damu yake atatwikwa yeye, lakini yeye aonyekaye ataiponya roho yake. Lakini kama mlinzi anaona, panga zikija, asipige baragumu, watu hawaonyeki; basi, panga zikija, zikimkamata mtu mmoja tu wa kwao, yeye atakamatwa kwa ajili ya manza, alizozikora, lakini damu yake nitamlipisha mlinzi. Wewe nawe, mwana wa mtu, nimekuweka kuwa mlinzi wa mlango wa Isiraeli, utakaposikia neno kinywani mwangu, sharti uwaonye na kuwaambia hilo neno langu. Nikimwambia asiyenicha: Wewe usiyenicha, utakufa kabisa, nawe humwambii neno hili la kumwonya asiyenicha, aiache njia yake, basi, yeye asiyenicha atakufa kwa ajili ya manza, alizozikora, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Lakini kama wewe ulimwonya asiyenicha kwa ajili ya njia yake na kumwambia, arudi na kuiacha hiyo njia yake, naye asiporudi na kuiacha hiyo njia yake basi, yeye atakufa kwa manza, alizozikora, lakini wewe utakuwa umeiponya roho yako. *Kwa hiyo, wewe mwana wa mtu, uambie mlango wa Isiraeli: Ninyi husema hivi kwamba: Tukitwikwa mapotovu yetu na makosa yetu, sisi tutazimia tu; hivyo tutawezaje kupata uzima? Waambie: Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, sipendezwi na kufa kwake asiyenicha, ila yeye asiyenicha, akirudi na kuiacha njia yake, apate uzima. Rudini! Rudini na kuziacha njia zenu mbaya! Kwa nini mnataka kufa, ninyi mlio mlango wa Isiraeli? Nawe mwana wa mtu, waambie wana wa ukoo wako: Wongofu wa mwongofu hautamponya siku, atakapofanya mapotovu, wala asiyenicha hataangushwa kwa hivyo, asivyonicha, siku atakaporudi na kunicha, wala mwongofu hatapata uzima kwa wongofu wake siku, atakapokosa. Nikimwambia mwongofu, ya kuwa atapata uzima, naye akiuegemea wongofu wake, afanye mapotovu, basi, wongofu wake wote hautakumbukwa tena, naye atakufa kwa ajili ya hayo mapotovu, aliyoyafanya. Tena nikimwambia asiyenicha: Utakufa kabisa, naye akirudi na kuyaacha makosa yake, afanye yaliyo sawa yaongokayo: yeye asiyenicha akirudisha aliyopewa ya kumwekea mtu, akilipa aliyoyanyang'anya watu, akiyafuata maongozi ya wenye uzima, basi, naye ataupata uzima wa kweli, asife kabisa. Makosa yake yote, aliyoyakosa, hayatakumbukwa tena; kwa kuwa amefanya yaliyo sawa yaongokayo, ataupata uzima wa kweli.* Wana wa ukoo wako husema: Njia ya Bwana hainyoki, lakini njia yao ndiyo isiyonyoka. Mwongufu akirudi na kuuacha wongofu wake, afanye mapotovu, atakufa kwa ajili yao. Tena asiyemcha Mungu akirudi, aje kumcha Mungu, afanye yaliyo sawa yaongokayo, basi, yeye atapata uzima. Mkisema: Njia ya Bwana hainyoki, kwa hiyo nitawapatiliza ninyi mlio mlango wa Isiraeli kila mtu, kama njia zake zilivyo. Ikawa katika mwaka wa 12 wa kuhamishwa kwetu siku ya tano ya mwezi wa kumi, ndipo, mtoro aliyetoka Yerusalemu aliponijia kuniambia: Umetekwa ule mji! Lakini mkono wake Bwana ulikuwa juu yangu jioni kabla ya kuja kwake yule mtoro, naye alinifumbua kinywa, mpaka yule akinijia asubuhi; ndivyo, nilivyofumbuliwa kinywa, nisiwe tena bubu kabisa. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, watu wayakaliayo yale mabomoko katika nchi ya Isiraeli husema kwamba: Aburahamu alikuwa mmoja tu, akaipata nchi hii, iwe yake; nasi tulio wengi tulipewa nchi hii, iwe yetu. Kwa hiyo waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Ninyi hula nyama zenye damu, tena huyaelekezea magogo yenu ya kutambikia macho yenu, tena humwaga damu za watu! Je? Hivyo mtaipata nchi hii, iwe yenu? Ninyi hujishikiza kwa panga zenu, hufanaya machukizo mkichafua kila mtu mke wa mweziwe! Je? Hivyo mtaipata nchi hii, iwe yenu? Sharti uwaambie hivi: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, wayakaliao yale mabomoko watauawa kwa panga, nao walioko shambani nitawatoa, waliwe na nyama wa porini, nao walioko vilimani ngomeni na mapangoni watakufa kwa magonjwa mabaya. Nitaigeuza nchi hii kuwa mapori yaliyo peke yao, niyakomeshe majivuno yao ya nguvu zao, milima ya Isiraeli itakapokuwa peke yao, kwa kuwa hatapapita mtu. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapoigeuza nchi hii kuwa mapori yaliyo peke yao kwa ajili ya machukizo yote, waliyoyafanya. Nawe mwana wa mtu, wana wao walio ukoo wako huzisimulia habari za kwako barazani namo milangoni mwa nyumba, husemezana kila mmoja na mwenziwe, kila mtu na ndugu yake kwamba: Njoni, msikie, kama ni neno gani lililotoka kwake Bwana! Hivyo wanakujia kama watu wanaojijilia tu, kisha wao walio ukoo wangu hujikalia mbele yako, wayasikilize maneno yangu, lakini hawayafanyi; kwa vinywa vyao husema maneno mazuri ya kupendeza, lakini kwa kufanya hao hushika mioyoni mwao njia za kupata faida tu. Tazama, wewe unakuwa kwao kama mtu mwenye sauti nzuri aimbaye wimbo wa kupendeza pamoja na kuupatanisha na marimba; huyasikia maneno yako, lakini hawayafanyi kabisa. Hapo, yatakapotimia, - nayo yatatimia kweli, - ndipo, watakapojua, ya kuwa ni mfumbuaji aliyekuwa katikati yao. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, wafumbulie wachungaji wa Isiraeli yatakayowapata! Wafumbulie wachungaji ukiwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Yatawapata, ninyi wachungaji wa Isiraeli mnaojichunga wenyewe! Tena sio kondoo wanaowapasa wachungaji, wawachunge? Lakini ninyi hula maziwa yenye mafuta, huvaa nguo za manyoya yao, huchinja walionona, lakini kuchunga hamwachungi kondoo. Walio wanyonge humkuwatia nguvu, waliougua hamkuwaponya, waliovunjika hamkuwafunga vitambaa, waliokimbizwakimbizwa hamkuwarudisha, waliopotea kabisa hamkuwatafuta, ila mmewatawala kwa nguvu na kwa ukorofi. Hivyo wametawanyika, kwa kuwa hawana mchungaji, wakawa chakula cha nyama wote wa porini, wakatawanyika. kondoo wangu wakatangatanga milimani po pote napo po pote penye vilima vinavyokwenda juu; ikawa hivyo, kondoo wangu wakitawanyika katika nchi yote nzima, lakini hakuwako wala aliyewauliza, kama wako wapi, wala aliyewatafuta. Kwa hiyo, ninyi wachungaji lisikieni neno la Bwana! Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, kweli kondoo wangu wamepokonywa, kondoo wangu wakawa chakula cha nyama wote wa porini, kwa kuwa hawana mchungaji, kwa kuwa wachungaji wangu hawakuwatafuta kondoo wangu, wakajichunga wenyewe, wasiwachunge kondoo wangu. Kwa hiyo, ninyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikiwajia wachungaji, niwatafute kondoo wangu mikononi mwao, niwakomeshe, wasiwachunge kondoo wangu tena, wasiweze tena kujichunga wenyewe; nitawaokoa kondoo wangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikiwatafuta mwenyewe kondoo wangu, niwakague. Kama mchungaji anavyowakagua kondoo wake siku, anapokuwa katikati yao kondoo waliotawanyika, hivyo nami nitawakagua kondoo wangu, nitawaponya na kuwatoa mahali po pote, walipotawanyika siku ile iliyokuwa yenye mawingu meusi. Nitawatoa kwenye makabila ya watu na kuwakusanya katika hizo nchi, niwapeleke katika hiyo nchi yao; ndiko, nitakakowachunga Waisiraeli milimani kwao namo mabondeni napo pote, watu wanapokaa katika hiyo nchi. Nitawachunga penye malisho mema, tena mazizi yao yatakuwa juu ya milima mirefu ya Waisiraeli; huko watalala katika mazizi mema, wakilisha malisho ya kuwanonesha katika milima ya Isiraeli. Mimi mwenyewe nitawachunga kondoo wangu, nami nitawalalisha; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Waliopotea nitawatafuta, nao waliokimbizwakimbizwa nitawarudisha, nao waliovunjika nitawafunga vitambaa, nao waliougua nitawatia nguvu; lakini wenye mafuta na wenye nguvu nitawaangamiza, niwachunge na kuwapatiliza. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Ninyi mliomo kundini mwangu mtaniona, nikiwaamua kondoo na kondoo, madume ya kondoo na ya mbuzi. Je? Haiwatoshi kulisha malisho mazuri, mkiyakanyagakanyaga kwa miguu yenu yaliyosalia malishoni penu? Mkinywa maji yaliyo safi nayo yaliyosalia mnayavurugiaje kwa miguu yenu? Kisha kondoo wangu wayalishe yaliyokanyagwakanyagwa na miguu yenu, tena wayanywe, mliyoyavuruga? Kwa hiyo Bwana Mungu aliye Mungu wenu anasema hivi: Mtaniona, nikiwaamua mwenyewe wale kondoo walionona nao hao kondoo waliokonda. Kwa kuwa mmewasukuma kwa mbavu na kwa mabega, mkawapiga kwa pembe zenu wote waliougua, mpaka mkiwatawanya huko nje; kwa hiyo mimi nitawaokoa kondoo wangu, wasipokonywe tena, nitakapoamua kondoo na kondoo. Ndipo, nitakapowainulia mchungaji mmoja, awachunge, ni mtumishi wangu Dawidi; yeye atawachunga, yeye atakuwa mchungaji wao. Nami Bwana nitakuwa Mungu wao, naye mtumishi wangu Dawidi atakuwa mkuu katikati yao; mimi Bwana nimeyasema. Ndipo, nitakapofanya nao agano la kuwapa utengemano, nitatowesha nyama wabaya wote katika hiyo nchi, wapate kukaa na kutulia hata nyikani, walale usingizi hata msituni. Nitawapatia mbaraka wao wenyewe nazo nchi zangu zenye vilima ziwazungukazo, nikizinywesha mvua, siku zake zitakapotimia; nazo hizo mvua zitakuwa mvua zenye mbaraka. Miti ya shambani itazaa matunda yao, nayo nchi itawapa mazao yake, watakaa katika nchi yao; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapoivunja miti ya makongwa yao na kuwaopoa mikononi mwao waliowatumikisha. Hawatatekwa tena na mataifa, wala hawataliwa na nyama wa nchi hiyo, watakaa salama, hatakuwako atakayewastusha. Nitaotesha kwao mashamba yatakayosifiwa kuwa mashamba, wasipatwe na njaa tena katika hiyo nchi, hawatatukanwa tena na wamizimu. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu wao, niko pamoja nao, nao watakuwa ukoo wangu; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Kwani ninyi m ukoo wangu, m kondoo wangu, ninaowachunga; ninyi m watu, nami ni Mungu wenu; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, ielekezee milima ya Seiri uso wako na kuifumbulia yatakayokuwa! Iambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikikujia, mlima wa Seiri; nitakukunjulia mkono wangu, nikugeuze kuwa mapori yaliyo peke yao! Miji yako nitaivunja, iwe mabomoko tu, nawe utakuwa mapori tu; ndipo, utakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Kwa kuwa umeshika uchukivu wa kale na kale, ukawabwaga wana wa Isiraeli kwenye panga siku zile, waliposhindwa, ni siku zile, walipolipishwa manza zao, walizozikora. Kwa hiyo Bwana Mungu anasema: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, nitaimwaga damu yako, nazo damu zitakukimbiza; kwa kuwa hukuchukiwa na kumwaga damu, damu zitakukimbiza. Nitaigeuza milima ya Seiri kuwa mapori yaliyo peke yao, nikitowesha kwao wapitaji wanaokwenda na kurudi. Milima yao nitaijaza mizoga yao waliouawa, katika vilima vyako na katika mabonde yako na katika makorongo lyako yote wataanguka waliouawa na panga. Nitakugeuza kuwa mapori ya kale na kale, miji yako isikae watu tena; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Kwa kuwa ulisema: Hayo mataifa mawili nazo nchi zao mbili zitakuwa zangu, tuzichukue! naye Bwama alikuwa yupo; kwa hiyo Bwana anasema: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, nitakufanyizia yayo hayo, uliyoyataka kuyafanya kwa makali yako na kwa wivu wako, uliyoyatenda kwa hivyo ulivyowachukia; ndipo, nitakapojulikana kwao, nitakapokuwa nimekwisha kukuhukumu. Ndipo, utakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Nimeyasikia maapizo yako yote, uliyoyasema na kuiapiza milima ya Isiraeli kwamba: Na iwe mapori, tupewe sisi kuila! Ndivyo, mlivyovikuza vinywa vyenu mbele yangu, nayo maneno yenu, mliyoyasema mbele yangu, yakawa ya majivuno tu; mimi nimeyasikia. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nchi yote nzima itafurahi, nitakapokugeuza kuwa mapori tu. Kama wewe ulivyofurahi, fungu lao walio mlango wa Isiraeli lilipogeuzwa kuwa mapori, hivyo ndivyo, nitakavyokufanyzia: utakuwa mapori tu, mlima wa Seiri, pamoja na nchi yote nzima ya Edomu; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Wewe mwana wa mtu, ufumbulie mlima wa Isiraeli yatakayokuwa, na kuiambia milima ya Isiraeli: Sikieni neno la Bwana! Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa adui wamesema na kuwabeza: Aha! Vilima vya kale na kale vimekuwa vyetu, tuvichukue! kwa hiyo yafumbue yatakayokuwa ukisema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kweli wamewageuza ninyi vilima kuwa mapori tu na kuwafokea pande zote, mwe vyao wa mataifa waliosalia, wawachukue, habari za kwenu zikasimuliwa na vinywa vyao vyenye ndimi mbaya, watu wakazinong'onezana. Kwa sababu hiyo, ninyi milima ya Isiraeli, sikieni neno la Bwana Mungu: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyoiambia milima iliyo mirefu nayo iliyo mifupi, hata makorongo na mabonde, nayo mabomoko na mapori, nayo miji iliyo mahame tu, iliyonyang'anywa na kuzomelewa na masao ya mataifa yaliyokaa na kuizunguka. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kweli itakuwa kwa moto wa wivu wangu, nikisema nao walio masao ya mataifa nao Waedomu wote waliojipa wenyewe nchi yangu, waichukue, iwe yao, wakafurahi kwa mioyo yote na kwa roho zenye mabezo walipowafukuza wa kwenu na kuwanyang'anya mali zao. Kwa hiyo ifumbulie nchi ya Isiraeli yatakayokuwa ukiiambia milima mirefu na mifupi, nayo makorongo na mabonde: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikisema kwa wivu na kwa makali yangu yenye moto, kwa kuwa mmejitwika yaliyowatia soni kwa wamizimu. Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Mimi nimeuinua mkono wangu, kwa hiyo itakuwa kweli: wamizimu wanaokaa na kuwazunguka watajitwika wenyewe yanayowatia soni. Lakini ninyi, milima ya Isiraeli, mtayachipuza matawi yenu, mzae nayo matunda yenu, kwa ajili yao walio ukoo wangu wa Isiraeli, kwani hao watakuja bado kidogo. Kwani mtaniona, nikija kwenu na kuwageukia, mpate kulimwa na kupandwa. Hata watu wengi nitawakalisha kwenu wa milango yote pia ya Isiraeli, miji yao ikaliwe tena, nayo mabomoko yajengwe tena. Nitakalisha kwenu watu wengi na nyama wengi, wazidi tena kwa kuzaa sana. Hivyo nitawapa kuwa wengi hapo, mtakapokaa kama siku zenu za kale, nitawafanyizia mema mengi kuliko siku za kwanza; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Kwenu nitawatembeza tena walio ukoo wangu wa Isiraeli, wawachukue, mwe tena fungu lao; hamtawaua tena wana wao. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa watu huwaambia ninyi: Wewe ndiwe mla watu, tena ndiwe muua watoto wa kwako, kwa hiyo hutakula mtu tena, wala hutawaua tena watoto wa kwako; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Sitaki, usikie kwako tena matusi ya wamizimu, wala hutajitwika tena yakutiayo soni kwa makabila ya watu, wala hutawakwaza tena watu wa kwako; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, walio mlango wa Isiraeli walipokaa katika nchi yao, waliitia uchafu kwa njia zao na kwa matendo yao; njia zao zilikuwa machoni pangu kama uchafu wa mwanamke mwenye siku zake. Nikawamwagia makali yangu yenye moto kwa ajili ya damu, walipozimwaga katika nchi hiyo, tena walipojipatia uchafu na magogo yao ya kutambikia. Nikawatawanya kwenye wamizimu na kuwatupatupa katika hizo nchi zao nilipowahukumu kwa hivyo, njia zao na matendo yao yalivyokuwa. Walipofika kwenye wamizimu wakalipatia Jina langu takatifu uchafu po pote, walipofika, watu wakisema kwa ajili yao: Hawa ndio walio ukoo wake Bwana, wametolewa katika nchi yao. Nikaona uchungu kwa ajili ya Jina langu takatifu, wale wa mlango wa Isiraeli walilolipatia uchafu kwenye mataifa po pote, walipofika. *Kwa hiyo uambie mlango wa Isiraeli: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Si kwa ajili yenu, ninyi na mlango wa Isiraeli, nikiwafanyizia hivyo, ila kwa ajili ya Jina langu takatifu, mlilolipatia uchafu kwenye wamizimu po pote, mlipofika. Nitalitakasa tena Jina langu kuu lililopatiwa uchafu kwenye wamizimu, mlilolipatia uchafu kwao; ndipo wamizimu watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapotakasika kwenu machoni pao; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Nitawachukua kwenye wamizimu nikiwakusanya na kuwatoa katika hizo nchi, niwarudishe katika nchi yenu. Nami nitawanyunyizia maji safi, ndipo, mtakapokuwa mmesafishwa; nitawasafisha, yawaondokee makosa yenu yote nayo magogo yenu yote, mliyoyatambikia. Nitawapa mioyo mipya, namo ndani yenu nitatia roho mpya, nitaitoa miilini mwenu ile mioyo iliyo migumu kama mawe, niwape mioyo iliyolegea kama nyama. Nayo roho yangu nitaitia ndani yenu, niwageuze kuwa watu wanaoyafuata maongozi yangu, wayashike mashauri yangu, wayafanye. Nanyi mtakaa katika hiyo nchi, niliyowapa baba zenu, mkiwa ukoo wangu, mimi nami nitakuwa Mungu wenu.* Nami nitawaokoa katika machafu yenu yote, kisha nitaziita ngano, nizizidishe kuwa nyingi, sitaleta tena njaa kwenu. Nayo matunda ya miti nitayazidisha kuwa mengi nayo mazao ya mashamba, kusudi msitiwe soni tena kwa wamizimu mkipatwa na njaa. Mtakapozikumbuka njia zenu mbaya na matendo yenu yasiyokuwa mazuri, ndipo, mtakapojichukia wenyewe machoni penu kwa ajili ya maovu yenu na machukizo yenu, mliyoyafanya. Ndivyo, asemavyo Bwana: Na ijulike kwenu, ya kuwa siwafanyizii hivyo kwa ajili yenu; sharti mwone soni na kuiva nyuso kwa ajili ya njia zenu, ninyi wa mlango wa Isiraeli. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Siku, nitakapowasafisha na kuwaondolea manza zote, mlizozikora, ndipo, nitakapoipatia miji yenu watu wa kukaa humo, nayo mabomoko yatajengwa tena. Nayo nchi iliyokuwa majani tu italimwa hapohapo palipokuwa mapori matupu machoni pao wote waliopapita. Ndipo, watakaposema: Nchi hii iliyokuwa mapori tu imegeuka kuwa kama bustani ya Edeni, nayo miji iliyokuwa mabomoko na mahame kwa kuvunjwa kwao sasa iko na maboma, nayo inakaa watu. Ndipo, wamizimu watakaosalia kwao wakaao na kuwazunguka watakapojua, ya kuwa mimi Bwana nimeyajenga yaliyovunjwa, nikayapanda yaliyokuwa mapori tu. Mimi Bwana nimeyasema, nami nitayafanya. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nalo hili nitawaitikia wao wa mlango wa Waisiraeli wakiniomba, niwafanyizie: Nitawazidisha kuwa watu wengi kama kondoo. Kama kondoo wa kutambika walivyo wengi, au kama mle Yerusalemu makundi ya watu yanavyokuwa mengi siku za sikukuu, ndivyo, miji iliyo mabomoko tu itakavyojaa makundi ya watu; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Mkono wa Bwana ukanishika, Bwana akanitoa kirohoroho, akanipeleka na kuniweka katikati ya hilo bonde, nalo lilikuwa limejaa mifupa. Akanipitisha po pote pande zote, ilipokuwa, nikaiona kuwa mingi sana humo bondeni juu ya mchanga, nami nikaiona kuwa mikavu sana. Akaniuliza: Mwana wa mtu, inakuwaje? Mifupa hii itaweza kuwa yenye uzima tena? Nikajibu: Bwana Mungu wewe unajua. Akaniambia: Ifumbulie mifupa hii yatakayokuwa! Iambie: Ninyi mifupa mikavu, sikieni neno la Bwana! Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyoiambia mifupa hii: Tazameni, nitawaletea pumzi ndani yenu, mpate kuwa wenye uzima tena. Nitatia mishipa juu yenu, tena nitaotesha nyama juu yenu, nitawafunika kwa ngozi, kisha nitawatia pumzi; ndipo, mtakapokuwa watu wazima, mtajua, ya kuwa mimi ni Bwana. Nikafumbua, kama nilivyoagizwa; ikawa, sauti ya kufumbua kwangu iliposikilika, pakawa na vishindoshindo, mifupa ikarudiana kila mfupa kwa mfupa mwenziwe. Nilipotazama, nikaona kwao mishipa, nazo nyama zikaja kuwa juu yao, kisha ngozi zikazifunika pande za juu, lakini pumzi hazikuwamo mwao. Akaniambia: Ufumbulie upepo! Fumbua, mwana wa mtu, ukiuambia upepo: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wewe upepo njoo na kutoka pande zote nne za upepo, uwapuzie hawa waliouawa, wapate kuwa wazima tena! Nikafumbua, kama nilivyoagizwa; ndipo, pumzi zilipowaingia, wakawa wazima, wakasimama kwa miguu yao, wakawa kikosi kikubwa sanasana. Akaniambia: Mwana wa mtu, mifupa hii ndiyo mlango wote wa Isiraeli. Tazama, husema: Mifupa yetu imekauka, kingojeo chetu kimepotea, tumekatwa roho. Kwa hiyo wafumbulie ukiwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikiyafunua makaburi yenu, niwatoe mle makaburini mwenu ninyi mlio ukoo wangu! Kisha nitawapeleka katika nchi ya Isiraeli. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu na kuwatoa mle makaburini mwenu ninyi mlio ukoo wangu. Nitawatia Roho yangu, mpate kuwa wazima tena, kisha nitawapeleka katika nchi yenu, mtulie huko; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, niliyoyasema ninayafanya; ndivyo, asemavyo Bwana. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, jipatie kijiti kimoja, ukiandike: Cha Yuda na cha wana wa Isiraeli walio wenziwe! Kisha jipatie kijiti kingine, ukiandike: Cha Yosefu! maana ni kijiti cha Efuraimu na cha mlango wa Isiraeli walio wenziwe! Kisha vibandike kimoja kwa mwenziwe, vishikamane kuwa kwako kijiti kimoja tu, hivyo viwili viwe kimoja kabisa mkononi mwako! Kama wana wao walio ukoo wako watakuuliza kwamba: Hutuambii maana yao hayo, uliyo nayo? waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona mimi, nikikichukua kijiti cha Yosefu kilichomo mkononi mwa Efuraimu nayo makabila ya Waisiraeli walio wenziwe, niwatie pamoja na kijiti cha Yuda, niwafanye kuwa kijiti kimoja tu; ndipo, watakapokuwa kimoja mkononi mwangu. Navyo vijiti, ulivyoviandika, sharti viwe mkononi mwako machoni pao. Kisha uwaambie: Hivi ndivyo Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikiwachukua wana wa Isiraeli kwenye wamizimu, walikopelekwa, niwakusanye na kuwatoa pande zote; kisha nitawapeleka katika nchi yao. Huko nitawafanya kuwa kabila moja katika nchi hiyo kwenye milima ya Isiraeli. Naye mfalme wao wote atakuwa mmoja tu, hawatakuwa tena makabila mawili, wala hawatagawanyika tena kuwa nchi mbili zenye wafalme. Wala hawatajipatia uchafu tena kwa kuyatambikia yale magogo yao wala kwa kuyafanya machukizo yao na mapotovu yao yote; nami nitawaokoa na kuwatoa mahali pao pote palipowakosesha, niwatakase; ndipo, watakapokuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Naye mtumishi wangu Dawidi atakuwa mfalme wao, yeye peke yake atakuwa mchungaji wao wote; ndipo, watakapoyafuata mashauri yangu na kuyashika maongozi yangu, wayafanye. Hivyo watakaa katika nchi hiyo, niliyompa mtumishi wangu Yakobo, waliyoikaa baba zenu; ndiko, watakakokaa wao na wana wao na wajukuu wao kale na kale, naye mtumishi wangu Dawidi atakuwa mfalme wao kale na kale. Nitafanya nao agano la kuwapa utengemano, nalo litakuwa la kale na kale kwao; nami nitawapa kukaa na kuwa wengi, hata Patakatifu pangu nitapaweka, pawe katikati yao kale na kale. Hapo patakuwa Kao langu la kwao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa ukoo wangu. Ndipo, wamizimu watakapojua, ya kuwa mimi Bwana ndiye anayewatakasa Waisiraeli, Patakatifu pangu patakapokuwa katikati yao kale na kale. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Mwana wa mtu, uelekeze uso wako kumtazama Gogi katika nchi ya Magogi aliye mkuu wa Rosi na wa Meseki na wa Tubali, umfumbulie yatakayomjia, ukisema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikikujia wewe Gogi uliye mkuu wa Rosi na wa Meseki na wa Tubali. Nitakugeuza nikikutia hatamu katika taya zako, nikutoe katika nchi yako pamoja na vikosi vyako vyote, farasi nao wawapandao, wao wote watakuwa wamevaa nguo za urembo, nao watakuwa mkutano mkubwa wenye ngao kubwa na ndogo, nao wote watashika panga. Kwako unao Wapersia na Wanubi na Waputi, wao wote ni wenye ngao na kofia za vita. Wagomeri na vikosi vyao nao wa mlango wa Togarma wakaao kaskazini mbali sana na vikosi vyao, kweli ni makabila mengi, uliyo nayo. Jipangeni na kujiweka tayari, wewe na mikutano yako yote iliyokusanyika kwako, nawe uwe mlinzi wao! Siku zitakapopita nyingi, utakaguliwa; miaka iliyowekwa itakapokwisha, utakwenda katika nchi iliyopata nguvu tena kwa kupona madonda ya panga, ufike kwao waliokusanywa na kutolewa kwa makabila mengi, wakae tena katika milima ya Isiraeli, iliyokuwa siku zote mapori matupu. Wao ndio waliotolewa kwenye makabila mengine, wakae salama wote pamoja. Ndiko, utakakopanda, uwajie kama upepo wa chamchela, utaifunika hiyo nchi kama wingu, wewe na vikosi vyako vyote vya yale makabila mengi, uliyo nayo. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Siku ile yatakuingia moyoni mambo yatakayokuwazisha mawazo mabaya. Ndipo, utakaposema: Nitapanda kwenda katika nchi iliyo wazi, nitaingia kwenye watu wanaotulia, wanaokaa salama; wote wanakaa pasipo boma, hawajui makomeo wala milango. Huko utataka kuteka mateka na kunyang'anya mali za watu, uinulie mkono wako mahame yanayokaa watu tena, uteke watu waliokusanywa na kutolewa kwenye mataifa, waliojipatia tena ng'ombe na mali nyingine, wanaokaa katikati ya dunia. Wasaba na Wadedani na wachuuzi wa Tarsisi na masimba yao wenye nguvu watakuuliza: Je? Umekuja kuteka mateka na kunyang'anya mali za watu? Umeikusanya mikutano yako kuchukua fedha na dhahabu, kujipatia ng'ombe na mali nyingine za watu, kuteka mateka mengi? Kwa hiyo, mwana wa mtu, mfumbulie Gogi yatakayompata ukimwambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Siku hiyo, walio ukoo wangu wa Isiraeli watakapokaa salama, hutaijua? Ndipo, utakapoondoka mahali pako huko mbali kaskazini wewe na makabila mengi pamoja na wewe, wote ndio wapanda farasi, ni mkutano mkubwa na vikosi vingi. Utapanda kuwajia walio ukoo wangu wa Isiraeli, utaifunika nchi hiyo kama wingu. Siku zilizowekwa zitakapokwisha, nitakupeleka katika nchi yangu, kusudi wamizimu wapate kunijua mimi, nitakapojitokeza kuwa mtakatifu, nikikupatiliza, wewe Gogi, machoni pao. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kumbe si wewe, niliyemsema siku za kale kwa vinywa vya watumishi wangu, wale wafumbuaji wa Isiraeli, waliofumbua siku zile miaka kwa miaka, ya kuwa nitakupeleka wewe, uwajie? Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Siku ile, Gogi atakapoiingia nchi ya Isiraeli, ndipo, makali yangu yenye moto yatakaponipanda kuingia puani mwangu. Kwa wivu wangu na kwa moto wa machafuko yangu nasema: Siku hiyo itakuwa na tetemeko kubwa katika nchi ya Isiraeli. Kwa kuniona watatetemeka samaki wa baharini na ndege wa angani na nyama wa porini na vidudu vyote vitambaavyo katika nchi nao watu wote wanaokaa katika nchi; ndipo, milima itakapoporomoka, nayo magenge yataanguka, nayo maboma yote yataanguka chini. Kisha nitaziita panga katika milima yangu yote, zije kumpiga; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu; ndipo, upanga wa kila mtu utakapompiga ndugu yake. Nami nitampatiliza kwa magonjwa mabaya na kwa kumwaga damu zao, tena nitanyesha mvua ifurikayo maji na mvua ya mawe na ya moto uchanganyikao na mawe ya viberitiberiti; hizo mvua nitamnyeshea yeye na vikosi vyake na yale makabila mengi, aliyo nayo. Hivyo nitajitokeza kuwa mkubwa na mtakatifu, nijulikane machoni pa wamizimu wengi, nilivyo; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Nawe mwana wa mtu, mfumbulie Gogi yatakayompata na kusema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikikujia, Gogi uliye mkuu wa Rosi na wa Meseki na wa Tubali! Nitakugeuza na kukushika kwa kamba, nikutoe huko kaskazini mbali na kukupandisha, uende, mpaka nikufikishe kwenye milima ya Isiraeli. Nitakupiga, upindi wako uanguke mkononi mwako mwa kushoto, nayo mishale yako nitaiangusha mkononi mwako mwa kuume. Milimani kwa Waisiraeli utaanguka wewe na vikosi vyako vyote nayo makabila, uliyo nayo; nitakutoa, uliwe nao ngusu na wote wenye mabawa na nyama wa porini. Utaanguka penye mapori, kwani mimi nimeyasema; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Nayo nchi ya Magogi nitaitupia moto nao wakaao salama katika visiwa; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana. Lakini Jina langu takatifu watalijulisha kwao walio ukoo wangu wa Isiraeli, nami sitanyamaza tena, Jina langu takatifu likipatiwa uchafu; ndipo, wamizimu watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana aliye Mtakatifu kwao Waisiraeli. Ndivyo, asemavyo Bwana: Hayo mtayaona, yakija kutimia siku ileile, niliyoisema. Ndipo, wakaao katika miji ya Waisiraeli watakapotoka, wavitumie vile vyombo vya vita kuwa kuni za kuwasha moto, zile ngao ndogo na kubwa, nazo pindi na mishale, nazo rungu na mikuki, wataitumia kuwa kuni za moto miaka saba. Hawataokota kuni za moto mashambani, wala hawatazikata misituni, kwani vyombo vya vita vitakuwa kuni zao. Hivyo watateka vitu kwao walioviteka vitu vyao na kuwanyang'anya mali zao; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Siku hiyo nitampa Gogi mahali pa kaburi kwao Waisiraeli katika bonde la wapitaji lililoko upande wa maawioni kwa jua kwenye bahari, nayo makaburi hayo yatawakinga wapitaji; ndiko, watakakomzika Gogi nao watu wake waliokuwa wengi, kisha watapaita Bonde la Wingi wa Gogi. Nao wa mlango wa Isiraeli watawazika muda wa miezi saba, kusudi waondoe uchafu katika nchi hiyo. Nao watu wote wa nchi hiyo watakuwa wakizika; hivyo watajipatia jina la kuwasifu siku ile, nitakapojitukuza; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Kisha watachagua watu wa kushika kazi hiyo siku zote, watembee katika nchi, wawazike wapitaji wale waliosazwa juu ya nchi, wauondoe uchafu huo. Ile miezi saba itakapopita, ndipo, watakapochunguza, watembezi wakitembea katika hiyo nchi; napo hapo, watakapoona mifupa ya mtu, watapajenga kando yake kichuguu, mpaka wazishi wamzike katika Bonde la Wingi wa Gogi. Hata mji utakaokuwako utaitwa Hamona (Wingi wa Watu). Hivyo ndivyo, watakavyoundoa huo uchafu wa hiyo nchi. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nawe mwana wa mtu, waambie ndege wote wenye mabawa nao nyama wote wa porini: Kusanyikeni! Njoni mkitoka pande zote, mkutane penye ng'ombe zangu za tambiko, nitakazowachinjia kuwa karamu kubwa ya nyama za tambiko milimani kwa Waisiraeli, mle nyama na kunywa damu! Mtakula nyama za wapiga vita wenye nguvu, mtakunywa damu za wakuu wa nchi, ndio madume ya kondoo na wana kondoo na mbuzi na ng'ombe, wote ni manono ya Basani. Mtakula mafuta, mshibe, mtakunywa damu, mlewe kwa hizo ng'ombe zangu za tambiko, nitakazowachinjia. Mtashiba mezani pangu kwa nyama za farasi nazo zao waliowapanda, kwa nyama za wapiga vita wenye nguvu nazo zao wote waliojiendea tu kupigana; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Ndivyo, nitakavyoutokeza utukufu wangu kwa wamizimu, nao wamizimu wote watayaona mapatilizo yangu, nitakayowapatia, nao mkono wangu, nilioutoa kuwakamata. Ndipo, walio mlango wa Isiraeli watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu wao, tangu siku ile hata siku zitakazokuja. Nao wamizimu watajua, ya kuwa walio mlango wa Isiraeli walihamishwa kwa ajili ya manza, walizokora walipoyavunja maagano yangu; kwa hiyo naliuficha uso wangu, wasiuone, nikawatia mikononi mwao waliowasonga, wao wote wauawe kwa panga. Hivyo, walivyojipatia uchafu kwa mapotovu yao, ndivyo, nilivyowafanyizia nilipouficha uso wangu, wasiuone. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Sasa nitayafungua mafungo yake Yakobo, niwahurumie wote walio mlango wa Isiraeli kwa kutenda wivu kwa ajili ya Jina langu takatifu. Nao watashikwa na soni iwapasayo kwa hivyo, walivyoyavunja maagano yangu yote, watakapokaa salama katika nchi yao, kwani hatakuwako atakayewastusha. Nitakapowarudisha kwao na kuwatoa kwenye makabila mengine na kuwakusanya, wazitoke nchi za adui zao, ndipo, nitakapojitokeza kwao kuwa Mtakatifu machoni pa wamizimu wengi; nao watajua, ya kuwa mimi Bwana Mungu wao kweli naliwahamisha kwenda kwa wamizimu, lakini nitawakusanya tena, warudi katika nchi yao, sitasaza hata mmoja wao huko. Wala sitauficha uso wangu tena, wasiuone, kwani nitawamwagia walio mlango wa Isiraeli Roho yangu; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Ikawa katika mwaka wa 25 wa kuhamishwa kwetu, mwaka ulipoanza, siku ya kumi ya mwezi, nao ulikuwa mwaka wa 14 wa kutekwa kwa huo mji, siku ileile ndipo, mkono wa Bwana uliponishika, ukanipeleka huko. Katika maono ya Kimungu akanipeleka katika nchi ya Waisiraeli, akaniweka katika mlima mrefu sana, nitulie huko; upande wake wa kusini kulikuwako yaliyofanana na majengo ya mji. Alipokwisha kunipeleka huko, mara nikaona mtu, akaonekana kuwa kama wa shaba, mkononi mwake alishika kamba ya katani na mwanzi wa kupimia, naye alikuwa amesimama langoni. Akaniambia yule mtu: Mwana wa mtu, tazama kwa macho yako, tena sikiliza kwa masikio yako! Nao moyo wako uuelekeze kuyaangalia yote, nitakayokuonyesha! Kwani umeletwa huku, kusudi uonyeshwe mambo; yote, utakayoyaona huku, uwatangazie walio ukoo wa Isiraeli! Nikaona ukuta wa nje ulioizunguka Nyumba pande zote pia. Nao mwanzi wa kupimia ulikuwa mkononi mwake yule mtu, ulikuwa wa mikono sita kama mkono wa mtu na upana wa shubiri moja; akaupima upana wa ukuta, ulikuwa mwanzi mmoja, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mwanzi mmoja. Kisha akaenda kwenye jengo la lango lililoelekea maawioni kwa jua, akavipanda vipago vyake, akakipima kizingiti cha jengo la lango, upana wake ulikuwa mwanzi mmoja; kizingiti hiki kimoja kilikuwa kwa upana mwanzi mmoja. Nacho chumba kimoja urefu wake ulikuwa mwanzi mmoja nao upana wake vilevile mwanzi mmoja, tena katikati ya vyumba kulikuwa mikono mitano. Kizingiti cha jengo la lango lililokuwa penye ukumbi, lililoelekea nyumbani, kilikuwa nacho mwanzi mmoja. Akaupima ukumbi wa lile jengo la lango wa upande wa nyumbani, nao ulikuwa mwanzi mmoja. Akaupima nao ukumbi wa lile jengo la lango wa upande wa mbele, nao ulikuwa mikono minane, nayo miimo yake ilikuwa mikono miwili, nao lukumbi huo ulikuwa upande wa nyumbani. Navyo vyumba vya jengo la lango hili lililoelekea maawioni kwa jua vilikuwa vitatu upande wa huku, tena vitatu upande wa huko, kipimo cha hivi vitatu kilikuwa hicho kimoja, hata kipimo cha miimo ya huku na ya huko kilikuwa hicho kimoja. Akaupima upana wa hapo pa kuingia, langoni nao ulikuwa mikono kumi, urefu wa lile lango ulikuwa mikono kumi na mitatu. Mbele ya vile vyumba palikuwa pamekatwa mipaka, urefu wao wa juu upande wa huku mkono mmoja, nao upande wa huko vilevile mkono mmoja; kila chumba kilikuwa mikono sita upande wa huku na mikono sita upande wa huko. Kisha akalipima jengo la lango toka dari la chumba hata dari la lchumba cha ng'ambo mikono ishirini na mitano, mlango ukiuelekea mlango wenziwe. Akafanya nguzo za mikono sitini; penye hizo nguzo ua ulilizunguka jengo la lango pande zote. Toka hapo pa kuingia langoni mpaka upande wa mbele wa ukumbi wa lango la ndani ilikuwa mikono hamsini. Madirisha yenye vyuma yalikuwa kwenye vyumba na kwenye miimo upande wa ndani wa hilo jengo la lango po pote; nao ukumbi ulikuwa na madirisha po pote yaliyoelekea ndani. Penye nguzo palikuwa pamechorwa mitende. Kisha akanipeleka katika ua wa nje, nikaona huko vyumba, tena chini palikuwa pametengenezwa sakafu kuzunguka pande zote uani; hapo penye sakafu palikuwa na vile vyumba, navyo vilikuwa thelathini. Hiyo sakafu ilikuwa kando penye malango, ikalingana na urefu wa majengo ya malango, ndiyo sakafu ya ua wa chini. Akaupima upana toka upande wa ndani wa jengo la lango la ua wa chini mpaka upande wa mbele wa jengo la lango la ua wa ndani mikono mia; vilikuwa hivyo upande wa maawioni kwa jua na upande wa kaskazini. Nalo jengo la lango la ua wa nje lililoelekea kaskazini akalipima urefu wake na upana wake. Vyumba vyake vilikuwa vitatu upande wa huku, tena vitatu upande wa huko; nazo nguzo zake na ukumbi wake kipimo chao kilikuwa kilekile cha jengo la mlango la kwanza. Urefu wake ulikuwa mikono hamsini, nao upana wake ulikuwa mikono ishirini na mitano. Madirisha yake na ukumbi wake na machoro ya mitende kipimo chao kilikuwa kilekile cha jengo la lango lililoelekea maawioni kwa jua; kwa vipago saba watu wakalipandia, kisha ukumbi wake ulikuwa mbele yao. Tena kulikuwako jengo la lango la ua wa ndani lililoelekea sawasawa jengo la lango la upande wa kaskazini na jengo la lango la upande wa maawioni kwa jua, akapima toka lango hata lango mikono mia. Akaniongoza njia ya kwenda kusini, nikaona, hata katika hiyo njia ya kwenda kusini kulikuwako jengo la lango, akazipima nguzo zake na ukumbi wake, kipimo chao kilikuwa kilekile. Hata madirisha yalilizunguka hilo jengo la lango na ukumbi wake pande zote, kama yale madirisha mengine yalivyokuwa, nao urefu ulikuwa mikono hamsini, nao upana ulikuwa mikono ishirini na mitano. Napo hapo palikuwa na vipago saba vya kupapandia, nao ukumbi wake ulikuwa mbele yao, nao ulikuwa na machoro ya mitende kwenye nguzo zake upande wa huku na upande wa huko. Tena kulikuwako hata jengo la lango la ua wa ndani katika hiyo njia ya kwenda kusini, akapima toka lango hata lango katika hiyo njia ya kwenda kusini mikono mia. Akanipeleka katika ua wa ndani kwenye njia ya kwenda kusini, akalipima hilo jengo la lango la kusini, vipimo vyake vilikuwa vile vile, Navyo vyumba vyake na nguzo zake na ukumbi wake vipimo vyao vilikuwa vilevile. Hata madirisha yalilizunguka hilo jengo la lango na ukumbi wake pande zote; nao urefu ulikuwa mikono hamsini, nao upana ulikuwa mikono ishirini na mitano. Pande zote palikuwa na vyumba, urefu ulikuwa mikono ishirini na mitano, nao upana ulikuwa mikono mitano. Ukumbi wake uliuelekea ua wa nje, nayo machoro ya mitende yalikuwa penye nguzo zake, tena hapo palikuwa na vipago vinane vya kupapandia. Kisha akanipeleka katika ua wa ndani penye njia ya maawioni kwa jua, akalipima jengo la lango vipimo vyake vilikuwa vilevile. Navyo vyumba vyake na nguzo zake na ukumbi wake vilikuwa vilevile. Hata madirisha yalilizunguka hilo jengo la lango na ukumbi wake pande zote. Urefu ulikuwa mikono hamsini, nao upana ukikuwa mikono ishirini na mitano. Ukumbi wake uliuelekea ua wa nje, nayo machoro ya mitende yalikuwa penye nguzo zake upande wa huku na upande wa huko, napo hapo palikuwa na vipago vinane vya kupapandia. Kisha akanipeleka penye jengo la lango la kaskazini, akalipima, vipimo vyake vilikuwa vilevile. Vyumba vyake na nguzo zake na ukumbi wake ni vivyo hivyo, nayo madirisha yalilizunguka pande zote; urefu ulikuwa mikono hamsini, nao upana ulikuwa mikono ishirini na mitano. Ukumbi wake uliuelekea ua wa nje, nayo machoro ya mitende yalikuwa penye nguzo zake upande wa huku na wa huko, napo hapo palikuwa na vipago vinane vya kupapandia. Hapo palikuwa na chumba, pake pa kuingilia palikuwa ukumbini mwa hayo malango, ndimo walimozisafishia nyama za kuteketezwa nzima za tambiko. Mle ukumbini mwa jengo la lango mlikuwa na meza mbili upande wa huku, tena meza mbili upande wa huko; ndipo, walipoziandalia ng'ombe za tambiko zilizochinjwa za kuteketezwa nzima nazo za weuo nazo za upozi. Tena upande wa nje pa kupandia napo pa kuliingilia jengo la lango la kaskazini palikuwa na meza mbili, nao upande mwingine wa ukumbi wa hilo jengo la lango palikuwa na meza mbili tena. Pamoja zilikuwa meza nne upande wa huku na meza nne upande wa huko kando ya hilo jengo la lango, zote pamoja zilikuwa meza nane; ndipo, walipoziandalia nyama zilizochinjwa. Tena palikuwa na meza nne za nyama za tambiko zilizoteketezwa nzima, zilijengwa kwa mawe yaliyochongwa, urefu wao ulikuwa mkono mmoja na nusu nao upana ulikuwa mkono mmoja na nusu, nao urefu wa kwenda juu ulikuwa mkono mmoja; ndipo, walipoviweka vyombo vya kuchinjia nyama wa kuteketezwa nzima na nyama wengine wa tambiko. Upande wao wa ndani palikuwa pametiwa mambo, urefu wao shibiri moja pande zote; hizo meza zilikuwa za kuwekea nyama, walizomtolea Mungu. Upande wa nje wa kila jengo la lango la ndani palikuwa na vyumba vya waimbaji katika ua wa ndani, kimoja kando ya jengo la lango la kaskazini kilielekea kusini, kimoja kilikuwa kando yake jengo la lango la maawioni kwa jua, nacho kilielekea kaskazini. Akaniambia: Hiki chumba kinachoelekea kusini ni cha watambikaji wanaongoja zamu humu Nyumbani. Nacho chumba kinachoelekea kaskazini ni cha watambikaji wanaongoja zamu mezani pa kutambikia, ndio wana wa Sadoki, ndio wanaomkaribia Bwana peke yao katika wana wa Lawi, wamtumikie. Akaupima huo ua ulikuwa wenye pembe nne, urefu wake ulikuwa mikono mia, nao upana wake ulikuwa mikono mia. Nayo meza ya kutambikia ilikuwa mbele ya Nyumba. Akanipeleka penye ukumbi wa Nyumba, akaupima unene wa miimo ya huo ukumbi, ulikuwa mikono mitano upande wa huku, tena mikono mitano upande wa huko, nao upana wa lango ulikuwa mikono kumi na minne, nazo kuta za kando ya jengo la lango upande wa ndani zilikuwa mikono mitatu upande wa huku na mikono mitatu upande wa huko. Urefu wa ukumbi ulikuwa mikono ishirini, nao upana wake mikono kumi na miwili, tena hapo palikuwa na vipago vya kupapandia, tena penye miimo palikuwa na nguzo, moja upande wa huku na moja upande wa huko. Akanipeleka Patakatifu, akaipima miimo, upana ulikuwa mikono sita upande wa huku na mikono sita upande wa huko, ndio upana wa kuta za Nyumba. upana wa hapo pa kuingia ulikuwa mikono kumi napo hapo kando pa kuingia palikuwa mikono mitano upande wa huku na mikono mitano upande wa huko. Akaupima urefu wake, ulikuwa mikono arobaini, nao upana ulikuwa mikono ishirini. Akaingia chumba cha ndani, akaupima mwimo wa hapo pa kuingia ulikuwa mikono miwili, napo hapo pa kuingia palikuwa mikono sita, nao upana wa kando pa kuingia ulikuwa mikono saba. Kisha akaupima urefu wake, ulikuwa mikono ishirini, nao upana ulikuwa mikono ishirini, kama upande wa mbele wa Patakatifu ulivyokuwa. Akaniambia; Hapa ndipo Patakatifu Penyewe. Akaupima ukuta wa Nyumba, ulikuwa mikono sita; nao upana wa vyumba vya kando vilivyoizunguka Nyumba pande zote po pote ulikuwa mikono minne. Hivyo vyumba vya kando vilikuwa vitatu kwenda juu, kila kimoja juu ya kingine, tena vilikuwa kila mara thelathini kwenda mbele vikizunguka ukutani penye Nyumba kando, vipate kushikizwa humo, lakini havikushukizwa ndani ya ukuta wa Nyumba. Hivyo vyumba vya kando vilivyozunguka kila dari lao la juu viliongezwa kuwa vipana kuliko vya chini; kwa kuzunguka hivyo nayo Nyumba yenyewe, ulipoitazama nje, upande wake wa juu ulikwenda ukiongezwa pande zake zote. Mtu alipotaka kupandia vyumba vya juu alitoka penye vyumba vya chini, akapita penye vile vya kati, afike juu. Nilipoitazama Nyumba nikaona palipoinuka kuizunguka pande zote; ndipo, misingi ya vyumba vya kando ilipokuwa, urefu wao wa kwenda juu ulikuwa mwanzi mzima wa mikono sita mpaka juu ukingoni pake. Upana wa ukuta wa nje penye hivyo vyumba ulikuwa mikono mitano; napo katikati vile vyumba vya kando ya Nyumba vilipatiwa mahali pao. Napo mahali palipoizunguka Nyumba upana wake mpaka penye hivyo vyumba palikuwa po pote mikono ishirini. Milango ya kuviingilia vyumba vya kando uliwekwa mmoja upande wa kaskazini, tena mmoja upande wa kusini. Tena palikuwa mahali palipoachwa kujengwa kuizunguka Nyumba pande zote, upana wake ulikuwa mikono mitano. Nalo jengo lililokuwa hapo palipokatazwa watu, palipoelekea baharini upana wake ulikuwa mikono sabini, nao ukuta wa hilo jengo unene wake ulikuwa mikono mitano po pote kulizunguka, nao urefu wake mikono tisini. Akaipima Nyumba, urefu wake ulikuwa mikono mia, napo palipokatazwa watu na lile jengo na kuta zake pamoja urefu wao ulikuwa nao mikono mia. Nao upande wa mbele wa Nyumba napo palipokatazwa watu upande wa maawioni kwa jua upana wao nao ulikuwa mikono mia. Akaupima urefu wa lile jengo lililopaelekea hapo palipokatazwa watu, lililokuwa nyuma yake Nyumba, na baraza zake upande wa huku na upande wa huko, ulikuwa mikono mia. Upande wa ndani wa hiyo Nyumba nazo kumbi za uani navyo vizingiti vyao na madirisha yao yenye vyuma na baraza zao zilizozunguka katika madari yale matatu na kukielekea hicho kizingiti zilikuwa zimefunikwa po pote kwa mbao nyembamba chini, tena kando mpaka penye madirisha, napo penye madirisha kando palikuwa pamefunikwa hivyo. Hapo juu penye mlango napo penye Nyumba upande wa ndani na wa nje katika kuta zote kuzunguka po pote ndani na nje palikuwa sawa. Tena palikuwa pamechorwa Makerubi na mitende hivyo: katikati mtende, tena hapa Kerubi na hapo Kerubi, kila mwenye nyuso mbili: uso wa mtu uliuelekea mtende upande wa huku, nao uso wa simba uliuelekea mtende upande wa huko; yalikuwa yamechorwa hivyo penye Nyumba yote kuizunguka pande zote. Toka chini mpaka juu ya mlango palikuwa pamechorwa Makerubi na mitende penye ukuta wa Nyumba. Hapo Patakatifu miimo ilikuwa yenye pembe nne, napo Patakatifu Penyewe, nilipopatazama, pakaoneka kuwa vivyo hivyo. Tena palikuwa na meza ya kutambikia iliyotengenezwa kwa mbao, urefu wa kwenda juu ulikuwa mikono mitatu, nao urefu wake wa kwenda mbele ulikuwa mikono miwili; pembe zake zilikuwa zimetokea nje, nao upande wa chini kwa urefu wake wote ulikuwa wa mbao, nazo kuta zake vilevile, akaniambia: Hii Meza ndiyo iliyoko mbele ya Bwana. Palikuwa na milango miwili hapo Patakatifu, tena Patakatifu Penyewe. Hii milango miwili ilikuwa yenye mbao mbili zizungukazo, ambao mbili za mlango huu mmoja, tena mbao mbili za mlango ule mmoja. Napo penye milango hii ya Patakatifu palikuwa pamechorwa Makerubi na mitende, kama palivyochorwa kutani. Tena hapo upande wa mbele wa ukumbi wa nje palikuwa na baraza iliyotengenezwa kwa mbao za miti. Madirisha yenye vyumba na machoro ya mitende yalikuwa upande wa huku na upande wa huko penye kuta za ukumbi napo penye vyumba vya kando vya hiyo Nyumba napo penye zile baraza. Kisha akanipeleka katika ua wa nje penye njia ya kwenda kaskazini, akanipeleka penye vyumba vilivyopaelekea hapo palipokatazwa watu, tena vililielekea jengo lililoko upande wa kaskazini. Upande wa mbele urefu wake ulikuwa mikono mia hapo pa kuingia upande wa kaskazini, nao upana wake ulikuwa mikono hamsini. Kuielekea ile mikono ishirini ya ua wa ndani, tena kuielekea sakafu ya mawe ya ua wa nje palikuwa na baraza juu ya baraza penye madari matatu. Mbele ya hivyo vyumba palikuwa pa kupitia palipouelekea ua wa ndani; upana wake ulikuwa mikono kumi, nao urefu wake hiyo njia ulikuwa mikono mia moja, nayo milango ya zile baraza ilielekea kaskazini. Navyo vyumba vya juu vilikuwa vimekatwa kidogo kwa upana wao, kwani zilipunguzwa na zile baraza zilizopita mbele yao, vilikuwa vifupi kuliko vile vya chini na vya kati vya hilo jengo. Kwani vilikuwa vya madari matatu, nayo yalikuwa hayana nguzo kama nguzo za uani; kwa hiyo lvya juu vilipunguzwa upana toka chini kuliko vya chini na vya katikati. Tena palikuwa na kitalu nje kilichokwenda sawasawa na vile vyumba upande wa ua wa nje mbele ya vyumba, urefu wake ulikuwa mikono hamsini. Kwani urefu wa vyumba vilivyokuwa upande wa ua wa nje ulikuwa mikono hamsini, lakini vile vilivyokuwa upande wa Patakatifu urefu wao ulikuwa mikono mia. Chini yao hivyo vyumba palikuwa pa kuingia upande wa maawioni kwa jua, mtu akitoka katika ua wa nje. Sawasawa na hicho kitalu kilichokuwa hapo uani, lakini upande wa kusini, palikuwa na vyumba vilivyopaelekea hapo palipokatazwa watu na hapo penye jengo lile. Mbele yao palikuwa pa kupitia; ukipatazama, palikuwa na vyumba kama vile vya upande wa kaskazini, urefu wao na upana wao ni uleule, nazo njia zao zote za kutoka na mambo mengine yalikuwa yaleyale. Nayo milango yao ilikuwa kama milango ya vyumba vilivyoelekea kusini; pa kuingia palikuwa pembeni pa njia iliyokwenda mbele ya kitalu kilichokuwa sawa kama kile cha upande wa kaskazini, mtu akiishika ile njia ya upande wa maawioni kwa jua, afike hapo. Kisha akaniambia: Vyumba vya upande wa kaskazini, hata vyumba vya upande wa kusini vilivyopaelekea palipokatazwa watu, ndivyo vyumba vitakatifu; ndimo, watambikaji watakamokula vyakula vitakatifu vyenyewe, tena ndimo, watakamoviweka vipaji vitakatifu vyenyewe, vilaji vya tambiko na nyama za ng'ombe za tambiko za weuo nazo zao za upozi, kwani ndivyo vyumba vitakatifu. Watambikaji wakitaka kuingia humo, wasitoke Patakatifu na kupitia penye ua wa nje! Humo ndimo, wayaweke mavazi yao waliyoyavaa wakimtumikia Mungu, kwani nayo ni matakatifu. Sharti wavae mavazi mengine, kisha wapakaribie, watu walipo! Alipokwisha kuipima Nyumba upande wa ndani, akanitoa humo na kunipeleka nje penye jengo la lango lililoelekea maawioni kwa jua, akaipima pande zote kuizunguka. Akaupima upande wa maawioni kwa jua kwa ule mwanzi wa kupimia, nao ulikuwa wote pia mianzi mia tano kwa kupima na ule mwanzi. Akaupima upande wa kaskazini, nao ulikuwa wote pia mianzi mia tano kwa kupima na ule mwanzi. Akaupima upande wa kusini, nao ulikuwa mianzi mia tano kwa kupima na ule mwanzi. Akazunguka penye upande wa baharini, akaupima, nao ulikuwa mianzi mia tano kwa kupima na ule mwanzi. Alipopapima pande zote nne penye ukuta uliopazunguka, urefu wake ulikuwa po pote mia tano, nao upana wake ulikuwa mia tano kupatenga Patakatifu napo penye watu. Akaniongoza tena kwenda penye lile lango lililoielekea njia ya maawioni kwa jua. Nilipotazama mara nikaona, utukufu wa Mungu wa Isiraeli ukija katika njia itokayo maawioni kwa jua, nao uvumi wake ulikuwa kama uvumi wa maji mengi, nayo nchi iliangaza kwa utukufu wake. Ulionekana kuwa kama lile ono, nililoliona, ulikuwa kweli kama lile ono, nililoliona nilipokuja kuuangamiza huo mji; tena ulionekana kuwa kama lile ono, nililoliona huko kwenye mto wa Kebari, nikaanguka kifudifudi. Nao utukufu wa Bwana ukaja kuingia humo Nyumbani katika njia ya lango lililoielekea hiyo njia ya maawioni kwa jua. Ndipo, roho iliponichukua, ikanipeleka katika ua wa ndani, mara nikaona, utukufu wa Bwana ulivyoijaza Nyumba. Nikasikia aliyesema na mimi toka mle Nyumbani, tena kulikuwako mtu aliyesimama hapo, nilipokuwa. Akaniambia: Mwana wa mtu, hapa ndipo penye kiti changu cha kifalme napo penye nyayo za miguu yangu; ndipo, nitakapokaa kale na kale katikati ya wana wa Isiraeli. Walio wa mlango wa Isiraeli hawatalipatia tena Jina langu takatifu uchafu, wala wenyewe, wala wafalme wao, wala kwa ugoni wao, wala kwa mizoga ya wafalme wao watakapokufa, wakiviweka vizingiti vyao penye kizingiti changu nayo miimo yao kandokando penye miimo yangu, pakawa ukuta tu uliopatenga pangu na pao, wakalipatia Jina langu takatifu uchafu kwa machukizo yao, waliyoyafanya; ndipo, nilipowamaliza kwa makali yangu. Sasa ugoni wao watauondoa pangu pamoja na mizoga ya wafalme wao, nipate kukaa katikati yao kale na kale. Wewe mwana wa mtu, walio mlango wa Isiraeli uwapashe habari za Nyumba hii, wapatwe na soni, wayaache maovu yao, waliyoyafanya, kisha waupime vema ulinganifu wake. Nao watakapopatwa na soni, wayaache yale yote, waliyoyafanya, ndipo, utakapowajulisha umbo lake Nyumba hii, ilivyolinganywa, napo pa kuitokea napo pa kuiingilia, jinsi umbo lake lote pia lilivyo! Tena uwajulishe maongozi yalipasayo umbo lake lote na maonyo yake yote ukiyaandika machoni pao, waliangalie umbo lake lote na maongozi yote yalipasayo, wayafanye! Haya ndiyo maonyo yaipasayo hii Nyumba: Po pote penye mipaka yake izungukayo huku milimani juu ndipo Patakatifu penyewe. Yaangalieni haya maonyo yaipasayo Nyumba hii! Hivi ndivyo vipimo vyake pa kumtambikia Bwana vya kupapima kwa mikono, mkono ukiwa mkono wa mtu na upana wa shibiri: msingi ni mkono mmoja, nao upana wake ni mkono mmoja, tena pembeni pake panazunguka kitalu, urefu wake ni shibiri moja. Nao huu ndio urefu wa juu wa hapo pa kutambikia: toka msingi ulioko mchangani mpaka daraja ya chini ni mikono miwili, nao upana wake mkono mmoja; tena toka daraja hili dogo mpaka daraja kubwa ni mikono minne, nao upana wake mkono mmoja. Kisha kilima cha Mungu ni mikono minne, tena hapo jikoni pa Mungu palikuwa na pembe nne zilizoelekea juu. Nalo jiko la Mungu ni mikono kumi na miwili urefu wake, nao upana wake ni mikono kumi na miwili, pande zake nne ni sawa, zenye pembe nne. Lile daraja kubwa urefu wake ni mikono kumi na minne, nao upana wake ni mikono kumi na minne, pande zake nne ni sawa; nacho kitalu kinacholizunguka ni nusu ya mkono, nao msingi wake po pote ni mkono mmoja; navyo vipago vya kupapandia viko upande wa maawioni kwa jua. Kisha akaniambia: Mwana wa mtu, hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu: Haya ndiyo, ninayokuagiza kuyafanya siku ile, hapo pa kunitambikia patakapokwisha kutengenezwa, watoe juu yake ng'ombe za tambiko pamoja na kupanyunyizia damu. Ndipo, utakapotoa ndama ya ng'ombe ya kiume kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, uwape watambikaji wa Kilawi walio wa uzao wa Sadoki, maana ndio wanaonikaribia na kunitumikia; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Kisha sharti uchote damu katika damu yake, uinyunyizie pembe zake nne napo penye zile pembe nne za daraja napo penye kitalu kipazungukacho! Ndivyo, utakavyopaeua pamoja na kupapatia upozi. Kisha umchukue huyo ndama atakayekuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, umteketeze penye Nyumba hii hapo panapoitumikia kazi hii upande wa nje wa hapo Patakatifu. Siku ya pili sharti upeleke dume la mbuzi asiye na kilema, wapaeue hapo pa kutambikia kama walivyopaeua na kumtoa yule ndama. Utakapokwisha kupaeua, sharti upeleke ndama ya ng'ombe ya kiume asiye na kilema na dume la kondoo asiye na kilema. Hao uwapeleke wa kuwatoa usoni pa Bwana, kisha watambikaji wawamwagie chumvi na kumtolea Bwana kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima. Sharti ufanye hivyo siku saba, wakitoa kila siku dume la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ndama ya ng'ombe ya kiume na dume la kondoo; hao wote, watakaowatoa, sharti wawe nyama pasipo kilema. Sharti siku saba wapapoze hapo pa kutambikia na kupaeua hivyo. Ndivyo, watakavyopatakasa, pawe patakatifu. Watakapozimaliza hizo siku, basi, siku ya nane nazo siku zitakazokuwa zote watambikaji watolee hapo pa kutambikia ng'ombe zenu za tambiko za kuteketezwa nzima nazo za kushukuru; ndipo, nitakapopendezwa nanyi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Akanirudisha kwenda kwa jengo la lango la nje la Patakatifu lielekealo maawioni kwa jua, nalo lilikuwa limefungwa. Bwana akaniambia: Lango hili sharti likae limefungwa, lisifunguliwe, wala asiingie mtu humo, kwa kuwa Bwana Mungu wa Isiraeli aliingia humo; kwa hiyo liwe limefungwa. Naye atakayekuwa mkuu, yeye mkuu peke yake atakaa humu, ale chakula mbele ya Bwana, ataingia kwa njia ya ukumbi wa hilo jengo la lango, kisha atatoka kwa njia ileile. Kisha akanipeleka kwenda kwa jengo la lango la kaskazini la hiyo Nyumba. Nilipotazama nikaona, utukufu wake Bwana, ulivyoijaza Nyumba, nikaanguka kifudifudi. Bwana akaniambia: Mwana wa mtu, yaweke moyoni mwako utakayoyaona kwa macho yako nayo utakayoyasikia kwa masikio yako, yote nikayoyasema na wewe kwa ajili ya maongozi yote yaipasayo Nyumba ya Bwana na kwa ajili ya maonyo yake uyaweke moyoni mwako, ujue, mtakapoiingia Nyumba hii, napo pote, mtakapopatoka hapa Patakatifu. Nao walio mlango wa Isiraeli ulio mkatavu waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Ninyi mlio mlango wa Isiraeli, yaacheni machukizo yenu yote, mliyoyafanya! Kwani ni mengi. Mwalileta wageni wasiotahiriwa wala mioyo wala miili, wapaingie Patakatifu pangu, waipatie Nyumba yangu uchafu, mliponiletea chakula changu cha tambiko, cha mafuta na cha damu; hivyo ndivyo, mlivyolivunja Agano langu kwa kuyafanya hayo machukizo yenu yote. Wenyewe hamkutumika na kuushika utumishi wa vitakatifu vyangu, mkawaweka wao kuwa mahali penu watumishi wa kutumikia Patakatifu pangu. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mgeni yeyote asiyetahiriwa wala moyo wala mwili asipaingie tena Patakatifu pangu, ijapo awe mmoja wao wale wageni wote wakaao kwa wana wa Isiraeli katikati. Ila Walawi walioniacha na kujiendea mbali hapo, Waisiraeli walipopotea, watatwikwa manza zao, walizozikora, ndio wale waliopotea kwa kuniacha wakiyafuata magogo yao ya kutambikia. Hao watapatumikia Patakatifu pangu na kuyangoja malango ya Nyumba hii na kuwa watumishi wa humu Nyumbani; ndio watakaozichinja ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima nazo zile nyingine, watu watakazozitoa za tambiko; hapo ndipo, watakaposimama mbele yao, wawatumikie. Kwa kuwa waliwatumikia watu mbele ya magogo yao ya kutambikia, wakawakosesha hivyo walio mlango wa Isiraeli, wakore manza, kwa sababu hii nimewaapia kwa kuuinua mkono wangu kwamba: Watatwikwa manza zao, walizozikora; ndivyo, asemavyo Bwana. Lakini wasinikaribie na kufanya kazi za utambikaji, wala wasivikaribie vitakatifu vyangu vyenyewe; hivyo watashikwa na soni kwa kutwikwa machukizo yao, waliyoyafanya. Kwa hiyo nitawaweka kuwa watumishi wa kutumikia humu Nyumbani, waufanye utumishi wake wote na kazi zote zitakazofanyizwa humu. Lakini watambikaji wa Kilawi walio wana wa Sadoki, walioushika utumishi wa Patakatifu pangu, wana wa Isiraeli walipopotea na kuniacha, hao ndio watakaonikaribia, wanitumikie na kusimama mbele yangu, wakiniletea mafuta na damu; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Hao watapaingia Patakatifu pangu, waikaribie meza yangu wakinitumikia kwa kuushika utumishi wangu. Nao watakapoingia malangoni mwa ua wa ndani sharti wavae mavazi ya pamba, wasiwe na nguo zo zote za manyoya ya kondoo wakifanya kazi za utambikaji mle malangoni mwa ua wa ndani namo humu Nyumbani! Vichwani sharti wavae vilemba vya nguo za pamba, hata viunoni sharti wavae suruali za pamba, wasijifunge nguo zitoazo jasho. Lakini watakapotoka kwenda katika ua wa nje, ni ule ua wa nje, watu walipo, sharti wayavue mavazi yao, waliyoyavaa wakifanya kazi za utumishi, wayaweke katika vile vyumba vya Patakatifu, kisha wavae mavazi mengine, wasiwapatie watu utakatifu kwa hayo mavazi yao. Vichwa vyao wasivinyoe kabisa, wala wasiache mavunga, yakue kabisa, ila nywele zao za vichwani wazikatekate. Tena wote walio watambikaji wasinywe mvinyo watakapouingia ua wa ndani. Wala wasichukue mjane wala mwanamke aliyeachwa kuwa wake zao, ila waoe wanawali walio wa uzao wa mlango wa Isiraeli au mjane aliye mjane wa mtambikaji. Wawafundishe watu wangu kupambanua kilicho kitakatifu nacho kinachotumika kwa watu siku zote, tena wawajulishe kupambanua yaliyo machafu nayo yaliyotakata. Tena watu wakigombana, hao ndio wanaopaswa na kuwasimamia na kuwaamua, nao wawaamue kwa mashauri yangu. Sharti wayashike Maonyo yangu na maongozi yangu kwenye mikutano yote ya sikukuu zangu, nazo siku zangu za mapumziko sharti wazitakase! Mtu aliyekufa wasimkaribie, wasijipatie uchafu! Wajipatie uchafu tu kwa baba na mama na mwana wa kiume na wa kike na kwa ndugu na kwa umbu asiyeolewa bado. Atakapokwisha kueuliwa, wamhesabie tena siku saba! Kisha siku, atakapopaingia Patakatifu, auingie ua wa ndani kufanya kazi ya utumishi hapo Patakatifu, kwanza apeleke ng'ombe ya tambiko ya weuo; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Tena fungu litakalowapasa kuwa lao, basi, mimi nitakuwa fungu lao, kwa hiyo msiwape mali zo zote kwao Waisiraeli za kuzishika kuwa zao! Mimi ni mali zao za kuzishika kuwa zao. Vipaji vya tambiko nazo ng'ombe za tambiko za weuo na za upozi wao watazila, navyo vyo vyote vitakavyokuwa mwiko kwao Waisiraeli kuvila vitakuwa mali zao. Nayo malimbuko yote pia yanayotolewa kwa kuwa ya kwanza, navyo vipaji vyenu vyote vingine, mtakavyovitoa, vitakuwa mali zao watambikaji nao unga wenu wa kwanza wa kupika mikate mtawapa watambikaji, mbaraka izikalie nyumba zenu. Lakini kila nyama aliyekufa kibudu au aliyeraruliwa na nyama mwingine, watambikaji wasile, kama ni ya ndege au ya nyama. Mtakapopiga kura za kujigawanyia mafungu ya nchi hii, mtatoa kwanza katika nchi hii kipande cha kumpa Bwana kuwa Patakatifu, urefu wake uwe mianzi 25000, nao upana wake uwe mianzi 10000; hapo sharti pawe Patakatifu katika mipaka yake yote ipazungukayo! Ndani yake pakatwe mahali penye mianzi 500 pande zake nne zipazungukazo kuwa pake Patakatifu Penyewe; mahali hapo pazungukwe pande zote na uwanda wa mikono 50. Mahali hapo palipopimwa utapapima tena urefu wa mianzi 25000 na upana wa mianzi 10000, napo hapo ndipo pajengwe Patakatifu patakapokuwa Patakatifu Penyewe. Nchi hiyo itakuwa takatifu, iwe yao watambikaji wanaofanya kazi za utumishi wa Patakatifu wakimkaribia Bwana na kumtumikia; kwa hiyo mahali hapo patakuwa pao pa nyumba zao, napo patakuwa patakatifu penye hapo Patakatifu. Pengine penye urefu wa mianzi 25000 na upana wa mianzi 10000 patakuwa pao Walawi wanaofanya kazi za utumishi wa Nyumba hii; hapo patakuwa mali zao za kupashika kuwa pao pa kukaa penye matuo 20. Kisha mtatoa tena mahali penye upana wa mianzi 5000 na urefu wa mianzi 25000 kuwa pake mji, pawe kandokando ya kile kipande kitakatifu cha nchi; hapo patakuwa mali zao wote walio mlango wa Isiraeli. Naye mkuu mtampa huku na huko penye kile kipande kitakatifu napo penye pake mji mbele ya kipande kitakatifu na mbele ya hapo palipo pake mji paelekeapo baharini upande wa kwenda baharini napo paelekeapo maawioni kwa jua, urefu wake ulingane na urefu wa fungu moja wa mafungu ya mashina toka mpaka wa baharini hata mpaka wa nchi uelekeao maawioni kwa jua. Hapo patakuwa mali zake za kupashika kuwa pake kwa Waisiraeli, wakuu wangu wasiwakorofishe tena walio ukoo wangu, nayo nchi watawapa walio mlango wa Isiraeli ya kuyagawia mashina yake. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mabaya yenu, mliyoyafanya ninyi wakuu wa Isiraeli, ni mengi; kwa hiyo acheni ukorofi na unyang'anyi, mpige mashauri yaliyo sawa yaongokayo, msiwafukuze kwao tena walio ukoo wangu! ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Sharti mtumie mizani zilizo sawa na pishi zilizo sawa na vipimo vilivyo sawa. Pishi moja na vibaba vinne sharti viwe kipimo kimoja sawasawa, vibaba vinne vipate kuwa fungu la sita la frasila, vilevile pishi moja iwe fungu la sita la frasila; hivyo frasila itatumika ya kulinganisha vipimo. Tena fedha (sekeli) moja iwe thumuni nane, fedha 20 na fedha 25 na tena fedha 15 pamoja zitakuwa mane moja, ndio shilingi 240. Hivi ndivyo vipaji vyangu vinavyowapasa kuvitoa: nusu kibaba kwa kila frasila ya ngano, vilevile nusu kibaba kwa kila frasila ya mawele. Tena mafuta, mtakayoyatoa, ni haya: kwa kila frasila mbili za mafuta ni nusu kibaba, vibaba vinne vikihesabiwa kuwa fungu la sita la frasila, kwani pishi sita ni frasila. Tena mwana kondoo mmoja kwa kila mia mbili za kondoo au za mbuzi walioko kwenye malisho ya Waisiraeli yanayonyweshwa. Haya yote ni ya vilaji vya tambiko na ya ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kushukuru na za kuwapatia watu upozi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Watu wote pia wa nchi hii wanapaswa na kuvitoa vipaji hivi vya kumpa aliye mkuu kwa Waisiraeli. Tena mkuu ndiye anayepaswa na kuzitoa ng'ombe za tambiko na vilaji na vinywaji vya tambiko penye sikukuu napo penye miandamo ya mwezi napo penye siku za mapumziko; kila mara walio mlango wa Isiraeli wanapokusanyikia, yeye ndiye atakayetoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima nazo za kushukuru, awapatie upozi walio mlango wa Isiraeli. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Katika mwezi wa kwanza siku ya kwanza uchukue ndama ya ng'ombe ya kiume asiye na kilema, upaeue Patakatifu! Mtambikaji achukue damu yake hiyo ng'ombe ya weuo, aipake mihimili ya Nyumba hii nazo pembe nne za daraja la hapo pa kutambikia, hata mihimili ya lango la ua wa ndani. Hivyo utavifanya hata siku ya saba ya huo mwezi kwa ajili ya mtu akosaye kwa kupotea au kwa ujinga tu. Ndivyo, mtakavyoieua Nyumba hii. Katika mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne sharti mfanye Pasaka, ndiyo sikukuu ya siku saba, inapoliwa mikate isiyotiwa chachu. Siku hiyo mkuu atoe kwa ajili yake na kwa ajili ya watu wote wa nchi hii ndama kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. Kisha hizo siku saba za sikukuu hii amtolee Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, ni ndama saba wa kiume na madume saba ya kondoo wasio na kilema, kila siku hizo siku saba, tena kila siku dume la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo. Tena sharti atolee kila ndama frasila moja ya unga kuwa kilaji cha tambiko, hata kila dume la kondoo vilevile, pamoja na pishi moja na nusu ya mafuta kwa kila frasila ya unga. Siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, kwa kuwa ni sikukuu ya Vibanda, afanye vivyo hivyo siku zake saba, akitoa ng'ombe za tambiko za weuo na za kuteketezwa nzima na vilaji vya tambiko pamoja na mafuta. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Lango la ua wa ndani lielekealo maawioni kwa jua sharti liwe limefungwa siku sita za kazi, lakini siku ya mapumziko lifunguliwe, hata siku ya mwandamo wa mwezi lifunguliwe. Mkuu akiingia penye ukumbi wa hilo lango toka nje, asimame hapo penye mhimili wa hilo lango, watambikaji waitengeneze ng'ombe yake ya tambiko ya kuteketezwa nzima nazo ng'ombe za tambiko za kushukuru, naye amwangukie Mungu penye kizingiti cha hilo lango, kisha atoke; kisha lango hilo lisifungwe mpaka jioni. Nao watu wa nchi hii wamwangukie Bwana hapo pa kuliingilia hilo lango siku za mapumziko na za miandamo ya mwezi. Nazo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, mkuu atakazomtolea Bwana siku za mapumziko, ziwe wana kondoo sita wasio na kilema na dume mmoja asiye na kilema. Tena kilaji cha tambiko kiwe frasila moja ya unga kwa yule dume, lakini kwa wana kondoo kiwe, kama mkono wake utakavyotoa, tena pishi moja na nusu ya mafuta kwa kila frasila moja ya unga. Siku ya mwandamo wa mwezi atatoa ndama ya ng'ombe ya kiume asiye na kilema na wana kondoo sita na dume moja, wote sharti wawe pasipo kilema. Frasila moja ya unga kwa yule ndama, tena frasila moja ya yule dume la kondoo iwe kilaji cha tambiko, nacho cha wana kondoo kiwe, kama mkono wake utakavyoleta, tena kwa kila frasila ya unga pishi moja na nusu ya mafuta. Mkuu akiingia aingie kwa njia ya ukumbi wa hilo lango, hata kutoka atoke kwa njia hiyohiyo. Lakini watu wa nchi hii wakimtokea Bwana kumwangukia penye mikutano ya sikukuu, wao walioingia katika lango la kaskazini sharti watoke penye lango la kusini, nao walioingia katika lango la kusini sharti watoke penye lango la kaskazini, mtu asirudi kwa njia ya lango lile, aliloliingia, ila atoke kwa lile la ng'ambo. Naye mkuu ataingia pamoja nao, wakiingia, kisha atatoka, nao wakitoka. Penye sikukuu napo penye mikutano ya sikukuu kilaji cha tambiko kiwe frasila moja ya unga kwa kila ndama, vilevile frasila moja ya unga kwa kila dume la kondoo, lakini kwa wana kondoo kiwe, kama mkono wake utakavyotoa, tena pishi moja na nusu ya mafuta kwa kila frasila moja ya unga. Kama mkuu anataka kumtolea Bwana kwa kupenda mwenyewe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima au za kushukuru, basi, wamfungulie lile lango lielekealo maawioni kwa jua, azitoe ng'ombe zake za tambiko za kuteketezwa nzima nazo za kushukuru, kama anavyofanya siku za mapumziko, kisha atoke! Akiisha kutoka, na walifunge hilo lango. Nawe umtolee Bwana kila siku mwana kondoo wa mwaka mmoja asiye na kilema kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ufanye hivyo kila kutakapokucha! Hata kilaji cha tambiko sharti ukitoe kila kutakapokucha, kiwe pishi moja ya unga na vibaba viwili vya mafuta ya kumiminiwa katika huo unga uliopepetwa vizuri. Hiki kilaji cha tambiko cha Bwana kimeagizwa cha siku zote za kale na kale. Sharti mtoe mwana kondoo nacho hicho kilaji cha tambiko pamoja na mafuta yake kila kutakapokucha kale na kale. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kama mkuu anampa mmoja wao wanawe fungu la nchi yake, litakuwa lao hata wanawe, walishike, liwe fungu lao, walilolipata. Lakini kama anampa mmoja wao watumishi wake fungu la nchi yake, aliyoipata, litakuwa lake mpaka mwaka mkuu wa ukombozi; ndipo, litakaporudi kwake mkuu; ni wanawe tu watakaokaa na fungu lake, liwe lao. Tena mkuu asichukue fungu lililo la watu akiwakorofisha na kuwafukuza kwao. Lililo lake ni fungu lile tu, alilopewa kulishika, liwe lake, nalo ndilo, atakaloachia wanawe, kusudi walio ukoo wangu wasitawanyike, mtu akiweza kuondolewa katika fungu, alilolishika, liwe lake. Akanipeleka hapo pa kuingia palipokuwa kando ya lile lango la kuviingilia vile vyumba vitakatifu vya watambikaji vielekeavyo kaskazini; hapo nikaona mahali pembeni panapoelekea baharini. Akaniambia: Humu ndimo, watambikaji wanamopikia nyama za ng'ombe za tambiko za upozi nazo za weuo, tena ndimo, wanamochomea vilaji vya tambiko, kusudi wasivipeleke katika ua wa nje na kuwapatia watu utakatifu. Kisha akanitoa na kunipeleka katika ua wa nje, akanipitisha penye pembe zake nne za huo ua; ndipo, nilipoona penye kila pembe ya huo ua ua mwingine. Penye pembe zote nne za huo ua palikuwa na nyua zilizofungwa kwa ukuta, urefu wao ulikuwa mikono 40, nao upana 30, kipimo chao hizo nyua ni kimoja tu. Zote nne zilizungukwa na ukuta wa mawe; chini penye hizo kuta kuzizunguka zote palikuwa pametengenezwa majiko. Akaniambia: Hizi ndizo nyumba za wapishi, watumishi wa Nyumba hii walimopikia nyama za ng'ombe za tambiko za watu. Akanirudisha penye kuiingilia Nyumba hii, mara nikaona maji yaliyotoka chini ya kizingiti cha Nyumba hii kwenda upande wa maawioni kwa jua, kwani upande wa mbele wa Nyumba hii ulielekea maawioni kwa jua; nayo hayo maji yakachuruzika chini ya upande wa kuumeni wa Nyumba hii, kusini penye meza ya kutambikia. Akanitoa kwa njia ya lango la kaskazini, akanizungusha huko nje kwenda kwenye lango la nje lielekealo maawioni kwa jua, mara nikaona maji yaliyotiririka upande wake wa kuumeni. Yule mtu akatoka kwenda maawioni kwa jua akishika kamba ya kupimia mkononi, akapima mikono elfu, akanipitisha humo majini, yakafika penye viwiko vya miguu. Akapima elfu tena, akanipitisha humo majini, yakafika magotini; akapima elfu tena, akanipitisha humo majini, yakafika viunoni. Akapima elfu tena, yakawa mto, nami sikuweza kuupita, kwani maji yalikuwa yameingilia ndani sana, yakawa maji ya kuogelea, basi, yalikuwa mto usiopitika. Akaniuliza: umeona, mwana wa mtu? Kisha akanirudisha, nikienda kwa miguu kandokando ya mto. Niliporudi mara nikaona ukingoni penye mto huo miti mingi sana huku na huko. Akaniambia: Maji hayo yanatoka hapa kwenda katika nchi zilizoko upande wa maawioni kwa jua, yanashuka kwenda nyikani, yafike baharini. Tena hapo yatakapoingia baharini, yale maji ya huko yataonekana, ya kuwa yamegeuka kuwa mazuri. Ndipo, itakapokuwa, vinyama vyote vitambaavyo hapo po pote, maji ya mto huo yatakapofika, vitapata uzima, nao samaki watakuwa hapo wengi sana, kwani maji haya yatafika hapo; ndipo, watakapopona na kupata kuwapo po pote, mto huu utakapofika. Ndipo, wavuvi watakaposimama pwani pake toka En-Gedi (Chemchemi ya Wana mbuzi) mpaka En-Egilemu (Chemchemi ya Ndama), maana patakuwa mahali pa kuanikia nyavu; samaki wa hapo watakuwa wa namna zao, tena wengi sana kama samaki wa Bahari Kubwa. Lakini mabwawa na maziwa yaliyoko kando yake maji yao hayatageuzwa kuwa mazuri, yatatumiwa ya chumvi. Kando ya mto huu pande zake za huku na za huko patakuwa na miti yo yote ifaayo kuliwa, majani yao hayatanyauka, wala matunda yao hayatakwisha. Kila mwezi yatazaa malimbuko tena, kwani maji yao yanatoka Patakatifu; kwa hiyo matunda yao yatatumiwa kuwa chakula, nayo majani yake yataponya watu. Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Huu ndio mpaka wa nchi hiyo, mtakayojigawanyia kuwa mafungu yao yale mashina kumi na mawili ya Isiraeli, Yosefu tu apate mafungu mawili. Mtajigawanyia mafungu yaliyo sawasawa kwa kila mtu na ndugu yake, yawe yenu, kwa kuwa niliapa na kuuinua mkono wangu ya kwamba: Nitawapa baba zenu; kwa hiyo nchi hii itawaangukia kuwa mafungu yenu. Nao huu ndio mpaka wa nchi hiyo: upande wa kaskazini toka kwenye Bahari Kubwa unakwenda Hetiloni kufika Sedadi, Hamati, Berota, Siburemu ulioko katikati ya mpaka wa Damasko na mpaka wa Hamati na Haseri wa kati ulioko kwenye mpaka wa Haurani. Ndivyo, mpaka utakavyotoka baharini kwenda mpaka Hasari-Enoni, mpaka wa Damasko uwe upande wa kaskazini, nao mpaka wa Hamati ukae kaskazini. Huu ndio mpaka wa kaskazini. Nao mpaka wa maawioni kwa jua uufuate mto wa Yordani toka Damasko na Haurani, tena toka Gileadi na nchi ya Isiraeli; huu mpaka mwupime toka hapo hata bahari ya maawioni kwa jua, uwe mpaka wa maawioni kwa jua. Nao upande wa kusini uelekeao kwenye jua kali uanzie Tamari kwenda Kadesi kwenye Maji ya Magomvi, kisha ufuate ule mto unaoingia katika Bahari Kubwa; huu ndio mpaka wa kusini uelekeao kwenye jua kali. Nao upande wa baharini mpaka ni Bahari Kubwa toka hapo kufika ng'ambo ya Hamati; huu ndio mpaka wa upande wa baharini. Nchi mtajigawanyia kwa mashina ya Isiraeli. Hapo, mtakapoipigia kura za kujipatia mafungu yatakayokuwa yenu, sharti mwapatie nao wageni wakaao kwenu katikati waliozaa wana katikati yenu. Nao watakuwa kwenu kama wazalia waliomo miongoni mwa wana wa Isiraeli; kwa hiyo sharti wapigiwe kura pamoja nanyi za kujipatia mafungu yatakayokuwa yao katikati ya mashina ya Waisiraeli. Kwa shina lilelile, mgeni atakakokaa, ndiko, mtakakompa fungu, liwe lake. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Haya ndiyo majina ya mashina: upande wa kaskazini kandokando ya njia ya Hetiloni kufika Hamati hata Hasari-Enani penye mpaka wa Damasko upande wa kaskazini kandokando ya Hamati ndiko kutakakokuwa fungu moja, la Dani toka upande wa maawioni kwa jua hata baharini. Kwenye mpaka wa Dani toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Aseri. Kwenye mpaka wa Aseri toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Nafutali. Kwenye mpaka wa Nafutali toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Manase. Kwenye mpaka wa Manase toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Efuraimu. Kwenye mpaka wa Efuraimu toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Rubeni. Kwenye mpaka wa Rubeni toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Yuda. Kwenye mpaka wa Yuda toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini kuwe fungu la kueuliwa, mtakalolitoa; upana wake uwe mianzi 25000, tena urefu uwe kama fungu moja jingine toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini; tena huko katikati kuwe na Patakatifu! Hata fungu la kueuliwa sharti mmtolee Bwana, urefu wake uwe mianzi 25000, tena upana wake uwe mianzi 10000. Hilo fungu takatifu litakuwa lao watambikaji, wapate mahali penye kaskazini, urefu wake uwe mianzi 25000, nako upande wa baharini upana uwe mianzi 10000, nako upande wa maawioni kwa jua upana uwe mianzi 10000, tena kusini urefu uwe mianzi 25000, nako huko katikati kuwe na Patakatifu pa Bwana. Fungu hilo liwe lao watambikaji waliotakaswa, walio wana wa Sadoki, walioyaangalia, niliyowaambia, wayaangalie; ndio wasiopotea hapo, wana wa Isiraeli walipopotea, kama Walawi walivyopotea. Kwa hiyo hapo patakuwa fungu lao, ni kipande cha lile fungu la kueuliwa lililo nchi takatifu yenyewe kwenye mpaka wa Walawi. Tena Walawi wapate kandokando ya mpaka wa watambikaji mahali penye urefu wa mianzi 25000, nao upana uwe mianzi 10000; urefu wote uwe mianzi 25000, nao upana wote uwe mianzi 10000. Lakini nchi hiyo wasiiuze kipande tu, wala wasiibadili kipande kwa nchi nyingine, kusudi nchi hii iliyo ya kwanza kwa uzuri wasiitie mikononi mwa mwingine, kwani ni nchi takatifu ya Bwana. Yale 5000 yatakayosalia kwa upana wa mianzi wa 25000 yawe mali ya huo mji wote, watu wapate pa kukaa na pa kulisha, huo mji wenyewe ukiwa katikati. Vipimo vyake viwe hivyo: upande wa kaskazini mianzi 4500, upande wa kusini mianzi 4500, upande wa maawioni kwa jua mianzi 4500, upande wa baharini mianzi 4500. Mahali pa mji pa kulisha pawe upande wa kaskazini mianzi 250, upande wa kusini mianzi 250, upande wa maawioni kwa jua mianzi 250, nako upande wa baharini mianzi 250. Kisha patasalia kwa urefu kandokando ya lile fungu takatifu la kueuliwa mahali penye mianzi 10000 kuelekea maawioni kwa jua, na mianzi 10000 kuelekea baharini, ndipo kandokando ya lile fungu takatifu la kueuliwa; mahali hapo mazao yake yaliwe nao watumikiao mle mjini. Hao watumikiao mle mjini watakuwa wa mashina yote ya Isiraeli, nao ndio watakaopalima hapo. Fungu lote la kueuliwa, mtakalolitoa, liwe mianzi 25000 kwa pande zote nne, ndipo patakapokuwa fungu takatifu la kueuliwa pamoja na hilo fungu litakalokuwa lake huo mji. Patakaposalia patakuwa pake mkuu upande wa huku na upande wa huko penye lile fungu takatifu la kueuliwa na penye lile fungu litakalokuwa lake huo mji kuifuata ile mianzi 25000 ya hilo fungu la kueuliwa mpakani kwenda upande wa maawioni kwa jua na upande wa baharini vilevile kuifuata ile mianzi 25000 kwenye mpaka uelekeao baharini sawasawa na mafungu mengine; hapo patakuwa pake mkuu. Hilo fungu takatifu la kueuliwa pamoja na Nyumba Takatifu itakuwa hapo katikati. Fungu lao Walawi nalo fungu lake mji, yote mawili yatakuwa katikati katika fungu lake mkuu; hilo fungu lake litakuwa katikati kwenye mpaka wa Yuda na kwenye mpaka wa Benyamini. Nayo mashina yaliyosalia mafungu yao ni haya: toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Benyamini. Kwenye mpaka wa Benyamini toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Simeoni. Kwenye mpaka wa Simeoni toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Isakari. Kwenye mpaka wa Isakari toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Zebuluni. Kwenye mpaka wa Zebuluni toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Gadi. Kisha mpaka wa Gadi upande wa kusini uelekeao kwenye jua kali utoke Tamari, ufike Kadesi penye Maji ya Magomvi, kisha ufuate mto kufika kwenye Bahari Kubwa. Hizo ndizo nchi, mtakazoyagawanyia mashina ya Isiraeli kwa kupiga kura kuwapatia mafungu yatakayokuwa yao. Hayo ndiyo mafungu yao makuu; ndivyo asemavyo Bwana Mungu. Pa kutokea mle mjini patakuwa hivyo: upande wa kaskazini utakuwa wa mianzi 4500. Nayo malango ya mji yataitwa kwa majina ya mashina ya Isiraeli. Malango matatu yataelekea kaskazini: lango moja la Rubeni, lango moja la Yuda, lango moja la Lawi. Nao upande wa maawioni kwa jua utakuwa wa mianzi 4500, nao utakuwa na malango matatu: lango moja la Yosefu, lango moja la Benyamini, lango moja la Dani. Nao upande wa kusini utakuwa wa mianzi 4500, nao utakuwa na malango matatu: lango moja la Simeoni, lango moja la Isakari, lango moja la Zebuluni. Nao upande wa baharini utakuwa wa mianzi 4500, nao utakuwa na malango matatu: lango moja la Gadi, lango moja la Aseri, lango moja la Nafutali. Kuuzunguka mji wote itakuwa njia yenye urefu wa mianzi 18000. Jina lake huo mji litakuwa toka siku ile: Bwana yumo. Katika mwaka wa tatu wa ufalme wa Yoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu, akausonga. Bwana akamtia Yoyakimu, mfalme wa Yuda, mkononi mwake, hata vyombo vinginevyo vya Nyumbani mwa Mungu akavipeleka katika nchi ya Sinari nyumbani mwa miungu yake, kisha akavipeleka hivyo vyombo katika nyumba ya vilimbiko vya miungu yake. Mfalme akamwambia Asipenazi aliyekuwa mkuu wa watumishi wake wa nyumbani, alete wana wa Kiisiraeli walio wa uzao wa kifalme na wa watu wenye macheo; achague wavulana wasio na kilema cho chote, wenye miili mizuri ya kupendeza, wenye ubingwa na ujuzi wote, wenye akili za kujua na za kutambua wanayoelezwa, wenye nguvu za kutumikia jumbani mwa mfalme, apate kuwafundisha maandiko na maneno ya Wakasidi. Mfalme akawaagizia siku ya siku vilaji vya urembo, yeye mfalme alivyovila, hata mvinyo, alizozinywa; akataka, wafugwe hivyo miaka mitatu, kisha wamtumikie mfalme. Katika hao wana wa Kiyuda walikuwamo Danieli na Hanania na Misaeli na Azaria. Naye mkuu wa watumishi wa nyumbani akawapa majina mengine: Danieli akamwita Beltesasari, naye Hanania akamwita Sadiraki, naye Misaeli akamwita Mesaki, naye Azaria akamwita Abedi-Nego. Lakini Danieli alisema moyoni mwake: Sitajipatia uchafu nikila vilaji vya urembo vya mfalme au nikinywa mvinyo zake; akamwomba mkuu wa watumishi wa nyumbani ruhusa, asijipatie uchafu hivyo. Mungu akampatia Daniel upendeleo na utu mbele yake mkuu wa watumishi wa nyumbani. Naye mkuu wa watumishi wa nyumbani akamjibu Danieli: Mimi ninamwogopa bwana wangu mfalme, aniagiziaye vilaji na vinywaji vyenu; kama angewaona ninyi, ya kuwa nyuso zenu zinanuna kuliko zao vijana wengine walio rika moja nanyi, basi, mtakuwa mmeniponza kwake mfalme, akanikata kichwa. Ndipo, Danieli aliposema na mtunza mvinyo, maana ndiye, mkuu wa watumishi wa nyumbani aliyemweka kuwasimamia akina Danieli na Hanania na Misaeli na Azaria, akamwambia: Tafadhali utujaribu sisi watumwa wako siku kumi tu, tupate maboga tu ya kula na maji tu ya kunywa! Kisha tutazamwe mbele yako, tulivyo, nao vijana wanaokula vilaji vya urembo vya mfalme watazamwe nao, walivyo. Kama utakavyoona, basi, ndivyo, utakavyotufanyizia sisi watumwa wako. Akawaitikia neno hili, akawajaribu siku kumi. Siku kumi zilipokwisha pita, wakatazamwa, wakaonekana kuwa wema, nayo miili yao ilikuwa imenona kuliko vijana wote waliovila vilaji vya urembo vya mfalme. Ndipo, mtunza mvinyo alipoviacha vile vilaji vya urembo na mvinyo, walizopewa za kunywa, akawapa maboga tu. Naye Mungu akawapa hawa vijana wanne akili za kujifunza ujuzi wote uliokuwamo katika vitabu, naye Danieli akampa kutambua maono na ndoto zote. Siku zilipokwisha pita, mfalme alizoziweka za kuwapeleka kwake, mkuu wa watumishi wa nyumbani akawapeleka kwake Nebukadinesari. Mfalme alipoongea nao, kwao wote hakuoneka aliyefanana nao akina Daniel na Hanania na Misaeli na Azaria; kwa hiyo wakapewa kumtumikia mfalme. Katika mambo yote ya ujuzi wa kutambua neno, mfalme aliyowauliza, akawaona, ya kuwa wanawashinda mara kumi waandishi na waaguaji wote waliokuwako katika ufalme wake. Danieli akawapo hata mwaka wa kwanza wa mfalme Kiro. Katika mwaka wa pili wa ufalme wake mfalme Nebukadinesari akaota ndoto, zikamhangaisha rohoni, kwa hiyo usingizi ukampotelea. Ndipo, mfalme alipoagiza kuwaita waandishi na waaguaji na waganga na Wakasidi, waje kumwambia mfalme maana ya ndoto zake. Wakaja, wakajipanga mbele yake mfalme. Mfalme akawaambia: Nimeota ndoto, roho yangu ikahangaika, ipate kuijua maana ya hiyo ndoto. Wakasidi wakamwambia mfalme kwa Kishami: E mfalme, na uwe mwenye uzima kale na kale! Waambie watumwa wako hiyo ndoto! ndipo, tutakapokueleza maana yake. Mfalme akawajibu, akawaambia Wakasidi: Neno langu lisilogeuzwa ni hili: msiponijulisha ndoto na maana yake, mtakatwa vipandevipande, nazo nyumba zenu zitabomolewa, ziwe vifusi. Lakini mkiweza kuieleza hiyo ndoto na maana yake, mtapata matunzo na vipaji na macheo makuu mbele yangu. Kwa hiyo ielezeni ndoto na maana yake! Wakajibu mara ya pili wakisema: Mfalme na awaambie watumwa wake ndoto! ndipo, tutakapoieleza maana. Mfalme akajibu kwamba: Mimi najua kweli, ya kuwa ninyi mnataka kujipatia siku, kwa kuwa mmeona, ya kama neno langu haligeuzwi. Kwani msipoijulisha hiyo ndoto, amri, nitakayoitoa kwa ajili yenu, ni ile moja; kwani mmepatana kuniambia maneno ya uwongo na ya madanganyo, mpaka siku nyingine zitokee. Kwa hiyo niambieni ile ndoto, nijue, ya kuwa mtanieleza nayo maana yake! Wakasidi wakamjibu mfalme kwamba: Hakuna mtu ulimwenguni anayeweza kulieleza hilo neno la mfalme; kwani hakuna mfalme ye yote, ingawa ni mkuu mwenye nguvu, aliyetaka jambo kama hilo kwao wote walio waandishi na waaguaji na Wakasidi. Jambo hili, mfalme analolitaka, ni zito, tena hakuna mtu awezaye kulieleza mbele yake mfalme, ni miungu tu, lakini haikai kwetu sisi tulio wenye miili ya kimtu. Ndipo, mfalme alipopatwa na machafuko makali sana, akaagiza, wajuzi wote wa Babeli wauawe. Amri hiyo ya kuwaua wajuzi ilipokwisha kutoka, wakamtafuta naye Danieli na wenziwe, wauawe. Ndipo, Danieli alipotumia akili zake zenye werevu, akasema na Arioki aliyekuwa mkuu wa walinzi wa mfalme, naye alikuwa ametoka kwenda kuwaua wajuzi wa Babeli. Basi, akamwuliza Arioki, kwa kuwa ni mtu wa nguvu wa mfalme: Mbona amri hiyo kali imetoka kwake mfalme? Arioki alipomjulisha Danieli jambo hilo, Danieli akaingia kwa mfalme, akamwomba, ampe siku kidogo, apate kumweleza mfalme maana ya ndoto. Kisha Danieli akaingia nyumbani mwake, akawajulisha wenziwe Hanania na Misaeli na Azaria hilo jambo, wamwombe Mungu wa mbinguni, awahurumie kwa ajili ya hilo jambo lililofichika, Danieli na wenziwe wasiuawe pamoja na wajuzi wa Babeli. Kisha Danieli akafumbuliwa katika ono la usiku hilo jambo lililofichika; ndipo, Danieli alipomtukuza Mungu wa mbinguni. Hivi ndivyo, Danieli alivyosema: Jina lake Mungu litukuzwe kale na kale! Kwani yeye ni mwenye ujuzi na uwezo! Yeye ndiye anayezigeuza siku na miaka, ndiye anayeondoa wafalme, tena ndiye anayeweka wafalme, ndiye anayewapa wajuzi ujuzi, nao watambuzi huwapa utambuzi. Yeye ndiye anayefunua yasiyochunguzika nayo yaliyofichwa. Anayajua yaliyomo gizani, nao mwanga unakaa kwake. Wewe Mungu wa baba zangu, mimi ninakushukuru na kukusifu, kwa kuwa umenipa ujuzi na uwezo, ukanijulisha tuliyokuomba, ukanijulisha lile jambo la mfalme. Ndipo, Danieli alipokwenda kwake Arioki, mfalme aliyemwagiza kuwaua wajuzi wa Babeli; alipofika akamwambia: Wajuzi wa Babeli usiwaue! Ila nipeleke kwake mfalme, nimweleze mfalme maana ya ndoto! Kisha Arioki akampeleka Danieli upesi kwake mfalme, akamwambia hivyo: Nimeona mtu, ni mmoja wao Wayuda waliotekwa na kuhamishwa kuja huku, ndiye atakayemjulisha mfalme maana ya ndoto. Mfalme akamwuliza Danieli aliyeitwa Beltesasari, akasema: Unaweza kunijulisha ndoto, niliyoiota, na kuniambia maana yake? Danieli akajibu masikioni pa mfalme, akasema: Fumbo, mfalme analolitaka, hakuna wajuzi wala waaguaji wala waandishi wala wachunguza nyota wanaoweza kumweleza mfalme maana yake. Lakini juu mbinguni yuko Mungu anayefunua mafumbo: yeye anamjulisha mfalme Nebukadinesari yatakayokuwa siku za mwisho. Ndoto yako na maono yaliyokuwa mbele yako, ulipolala kitandani, ndiyo haya: Wewe mfalme ulipolala kitandani, yakakuinukia mawazo ya mambo yatakayokuwa halafu; ndipo, yeye afunuaye mafumbo alipokujulisha yatakayokuwa. Mimi nami sikufunuliwa fumbo hilo kwa kwamba ninao ujuzi kuliko wengine walipo, ila ni kwa kwamba mfalme ajulishwe maana ya ndoto, upate kuyajua, uliyoyawaza moyoni. Wewe mfalme ulikuwa ukiota, mara ukaona kinyago kimoja. Kinyago hicho kilikuwa kikubwa sana, kikametuka kabisa, kikasimama mbele yako, kikatia woga kwa kutazamwa tu. Hicho kinyago kichwa chake kilikuwa cha dhahabu tupu, kifua chake na mikono yake ilikuwa ya fedha, tumbo lake na viuno vyake vilikuwa vya shaba, mapaja yake yalikuwa ya chuma, miguu yake ilikuwa nusu ya chuma, nusu ya udongo. Ulipokuwa unakitazama, mara jiwe likaporomoka lenyewe lisilotupwa na mikono ya watu, likakipiga kile kinyago penye miguu yake iliyokuwa ya chuma na ya udongo, likaiponda. Ndipo, yote pia yalipopondeka kwa mara moja, chuma, udongo, shaba, fedha, dhahabu, yakawa kama makapi penye kupuria ngano siku za kiangazi, upepo ukayapeperusha, yakatoweka kabisa, hata mahali pao hapakujulika. Lakini lile jiwe lililokiponda kile kinyago likawa mlima mkubwa, ukaieneza nchi yote. Hii ndiyo ndoto, sasa tumwambie mfalme nayo maana yake: Wewe mfalme ndiwe mfalme wa wafalme, Mungu wa mbinguni amekupa ufalme na uwezo na nguvu na macheo makuu. Pote panapokaa watu na nyama wa porini na ndege wa angani amepatia mkononi mwako, uwatawale hao wote. Wewe ndiwe kichwa cha dhahabu. Nyuma yako utatokea ufalme mwingine usio na nguvu kama wako. Kisha utafuata ufalme wa tatu, ni wa shaba utazitawala nchi zote. Kisha utakuwa ufalme wa nne wenye nguvu kama za chuma; kama chuma kinavyovunja na kuponda vyote kabisa, ndivyo, utakavyoponda na kuuvunja ufalme wote mwingine kama chuma chenye kuvunja. Lakini hivyo, ulivyoiona miguu yake na vidole vyake kuwa nusu yao ya udongo na nusu yao ya chuma, utakuwa ufalme uliogawanyika: upande utakuwa wenye nguvu za chuma, sawasawa kama ulivyoona chuma kilichochanganyika na udongo wa mfinyanzi. Navyo vidole vya miguu yake nusu yao ni ya chuma nusu yao nyingine ni ya udongo, ni kwamba: Upande wa ufalme huo utakuwa wenye nguvu, lakini upande utakuwa unavunjikavunjika. Tena umeona, chuma kilivyochanganyika na udongo wa mfinyanzi, ni kwamba: Wao watajichanganyachanganya na vizazi vya watu kwa kuoana, lakini hawataambatana mtu na mwenziwe, kama chuma kisivyochanganyikana na udongo. Siku zile za wafalme hao Mungu wa mbinguni atatokeza ufalme usioangamika kale na kale, usiochukuliwa tena na kabila jingine, nao utauponda ufalme wote mwingine na kuutowesha, lakini wenyewe utakaa kale na kale, kama ulivyoliona lile jiwe, likiporomoka toka mlimani lenyewe lisilotupwa na mikono ya watu, likaponda chuma na shamba na udongo na fedha na dhahabu. Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme yatakayokuwa siku zitakazokuja. Ndoto hii ni ya kweli kabisa, nayo maana yake inategemeka. Ndipo, mfalme Nebukadinesari alipoanguka kifudifudi, kisha akamwinamia Danieli, akaagiza kumtolea vipaji vya tambiko na uvumba. Kisha mfalme akamwambia Danieli akisema: Kweli Mungu wenu ni Mungu aipitaye miungu yote, ni Bwana wa wafalme, maana huyafunua yaliyofichwa, kwa hiyo umeweza kulifunua hili fumbo. Kisha mfalme akampa Danieli macheo na matunzo mazuri mno, mengi sana, akampa nalo jimbo lote la Babeli, alitawale, awe mkuu wao watawala nchi wa kuwaamrisha wajuzi wote wa Babeli. Danieli alipomwomba mfalme, akawaagizia akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego kazi ya kuliangalia jimbo la Babeli, naye Danieli akakaa jumbani mwa mfalme. Mfalme Nebukadinesari akatengeneza kinyago cha dhahabu, urefu wake ni mikono 60, nao upana wake ni mikono 6, akakisimamisha katika bonde la Dura katika nchi ya Babeli. Kisha mfalme Nebukadinesari akatuma wajumbe, awakusanye wenye amri na wakuu na watawala nchi na waamuzi na watunza mali na mabwana shauri na wandewa na wakuu wote wa nchi, waje kukieua kinyago hicho, mfalme Nebukadinesari alichokisimamisha. Ndipo, walipokusanyika wenye amri na wakuu na watawala nchi na waamuzi na watunza mali na mabwana shauri na wandewa na wakuu wote wa nchi kukieua kinyago hicho, mfalme Nebukadinesari alichokisimamisha, wakasimama mbele ya hicho kinyago, Nebukadinesari alichokisimamisha. Mpiga mbiu akatangaza kwa sauti ya nguvu kwamba: Ninyi makabila nanyi koo za watu walio wenye ndimi za watu mnaagizwa hivi: siku, mtakapozisikia sauti za mabaragumu na za filimbi na za marimba na za mapango na za mazeze na za mazomari na za namna zote za ngoma, sharti mwanguke kukisujudia kinyago cha dhahabu, mfalme Nebukadinesari alichokisimamisha. Kila mtu atakayekataa kuanguka na kukisujudia atatupwa papo hapo ndani ya tanuru iwakayo moto. Kwa sababu hii siku ile ilipofika, wao wote wa makabila ya watu walipozisikia sauti za mabaragumu na za filimbi na za marimba na za mapango na za mazeze na za namna zote za ngoma, basi, ndipo, makabila na koo zote za watu, wao wote wenye ndimi za watu walipoanguka wakikisujudia hicho kinyago cha dhahabu, mfalme Nebukadinesari alichokisimamisha. Kwa sababu hiyo siku zile wakaja waume wa Kikasidi wakawachongea Wayuda, wakamwambia mfalme Nebukadinesari hivyo: E mfalme, na uwe mwenye uzima kale na kale! Wewe mfalme umetoa amri kwamba: Kila mtu atakapozisikia sauti za mabaragumu na za filimbi na za marimba na za mapango na za mazeze na za mazomari na za namna zote za ngoma sharti aanguke na kukisujudia hicho kinyago cha dhahabu. Kila mtu atakayekataa kuanguka na kukisujudia atatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto. Basi, wako waume wa Kiyuda, uliowaagizia kazi ya kuiangalia nchi ya Babeli, ndio Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego; waume hao hawakuishika amri yako, mfalme, wala hawaitumikii miungu yako, wala hawakiangukii hicho kinyago cha dhahabu, ulichokisimamisha. Ndipo, Nebukadinesari alipokasirika na kuchafuka sana, akaagiza kuwaleta akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, kisha waume hawa wakapelekwa kwake mfalme. Nebukadinesari akawauliza kwamba: Ninyi Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, mnakataaje kuitumikia miungu yangu na kukiangukia hicho kinyago cha dhahabu, nilichokiweka? Kama ninyi mko tayari siku, mtakapozisikia sauti za mabaragumu na za filimbi na za marimba na za mapango na za mazeze na za namna zote za ngoma, mwanguke na kukisujudia kila kinyago cha dhahabu, nilichokitengeneza, basi; lakini msipokiangukia, mtatupwa papo hapo ndani ya tanuru iwakayo moto. Tena yuko Mungu gani atakayewaokoa mkononi mwangu? Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego wakajibu, wakamwambia mfalme: Nebukadinesari, kwetu sisi ni kazi bure kukujibu neno moja tu. Tazama, Mungu wetu, tunayemtumikia sisi, ndiye anayeweza kutuokoa katika tanuru iwakayo moto, namo mkononi mwako, mfalme, atatuokoa. Lakini ijapo hataki kutuokoa, uvijue, wewe mfalme: miungu yako sisi hatutaitumikia, wala kinyago cha dhahabu, ulichokisimamisha, hatutakiangukia. Ndipo, makali yenye moto yalipoushika moyo wote wa Nebukadinesari, nao uso wake ukawa mwingine kwa kuwaona akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, akaagiza kabisa kuwasha moto mkubwa katika tanuru kuupita moto wake wa siku zote mara saba. Kisha akaagiza watu walio wenye nguvu zaidi katika vikosi vyake, wawafunge akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, kisha wawatupe katika tanuru iwakayo moto. Kwa hiyo watu hawa wakafungwa pamoja na fulana zao na kanzu zao na shati zao na mavazi yao mengine, wakatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto. Kwa kuwa amri ya mfalme ilikuwa imetolewa kwa nguvu kabisa, ule ukali wa moto uliowaka sana ukawaua hao watu waliowachukua akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego. Lakini wale waume watatu, Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, wakaanguka ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamefungwa. Kisha mfalme Nebukadinesari akastuka, akainuka kwa upesi, akawaambia wasemaji wake wa shaurini kwamba: Je? Hatukutupa watu watatu ndani ya tanuru, nao walikuwa wamefungwa? Wakajibu, wakamwambia mfalme: Ndivyo kweli, mfalme. Akajibu akisema: Tena inakuwaje? Mimi ninaona watu wanne wasiofungwa kabisa, wanatembea motoni, tena hawaungui hata kidogo; naye wa nne sura yake anafanana na mwana wa Mungu. Kisha Nebukadinesari akalikaribia lango la tanuru iwakayo moto, akaita kwamba: Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego mnaomtumikia Mungu Alioko huko juu, tokeni nje! Ndipo, Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego walipotoka motoni. Wenye amri na wakuu na watawala nchi na wasemaji wa shaurini wa mfalme waliokuwa wamekusanyika hapo wakaona, ya kuwa moto haukuweza kuwafanyizia kitu watu hawa, nywele za vichwani pao hazikuungua, wala nguo zao hazikugeuka kuwa nyingine, wala mnuko tu wa moto haukuwapata. Nekukadinesari akasema kwamba: Na atukuzwe Mungu wao Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, kwa kuwa amemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtegemea wakikataa kuifuata amri ya mfalme, wakaitoa miili yao, kwamba wasiangukie mungu wo wote na kuusujudia, ila Mungu wao tu. Kwa hiyo sasa inatoka amri kwangu kwamba: Kwao makabila na koo zote, kwao wote wenye ndimi za watu, kila atakayesema neno la kumkosea Mungu wao Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego atakatwa vipandevipande, nayo nyumba yake itageuzwa kuwa kifusi, kwa kuwa hakuna Mungu mwingine anayeweza kuponya hivyo. Ndipo, mfalme alipowaongezea akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego macheo yao ya kuliangalia jimbo la Babeli. Mfalme Nebukadinesari akawaandikia makabila na koo zote, wao wote wenye ndimi za watu wanaokaa katika nchi yote nzima, kwamba: Utengemano wenu na uwe mwingi! Vielekezo na vioja, Mungu Alioko huko juu alivyonifanyia, imenipendeza kuvieleza. Vistaajabuni vielekezo vyake vilivyo vikuu! Navyo vioja vyake vilivyo vya nguvu! Ufalme wake ni ufalme wa kale na kale, nayo enzi yake ni ya vizazi na vizazi. Mimi Nebukadinesari nalitulia nyumbani mwangu, nikawapo na kufanikiwa katika jumba langu kuu. Nikaota ndoto iliyonistusha, nayo mawazo yaliyonijia, nilipolala kitandani, nayo maono ya macho yangu yakanitia woga. Amri ikatoka kwangu ya kuniletea wajuzi wote wa Babeli, wanijulishe maana ya ndoto. Kwa hiyo wakaniletea waandishi na waaguaji na Wakasidi na wachunguza nyota, mimi nikawaambia ndoto, lakini hawakunijulisha maana yake. Mwisho akatokea mbele yangu Danieli aliyeitwa Beltesasari kwa jina la mungu wangu, namo mwake imo roho ya miungu mitakatifu, nikamwambia ndoto nikisema: Beltesasari, mkuu wa waandishi, mimi ninakujua, ya kuwa roho ya miungu mitakatifu imo mwako, hakuna fumbo linalokusumbua; hii ni ndoto, niliyoiota, niambie maana yake! Maono niliyoyaona kwa macho yangu, nilipolala kitandani, ni haya: nilikuwa nikitazama, mara nikaona mti katika nchi, uliokuwa mrefu sana kwa kimo chake. Mti huo ukaendelea kukua na kupata nguvu, mpaka kilele chake kifike mbinguni, ukaonekana hata mapeoni kwa nchi. Majani yake yalikuwa mazuri, matunda yake yakawa mengi, vyakula vilivyopatikana kwake vikawatoshea watu wote pia, chini yake kivulini wakatua nyama wote wa porini, katika matawi yake ndege wa angani wakajenga viota vyao; hivyo wote wenye miili wakaushiba. Nilipokuwa ninautazama katika maono, niliyoyaona kwa macho yangu nilipolala kitandani, mara nikaona, mlinzi mtakatifu akishuka kutoka mbinguni. Akaita kwa sauti ya nguvu kwamba: Ukateni mti huu! Yachanjeni matawi yake! Majani yake yapukuseni! Matunda yake yatapanyeni, nyama wakimbie chini yake, hata ndege waondoke katika matawi yake! Majani yake yapukuseni! Matunda yake yatapanyeni, nyama wakimbie chini yake, hata ndege waondoke katika matawi yake! Lakini shina lenye mizizi yake liacheni mchangani, likiwa limefungwa kwa vyuma na kwa shaba katika mbuga yenye majani mabichi, liloweshwe na umande wa mbinguni, yale majani ya nchi yawe fungu lake, nalo lao nyama. Moyo wake utageuzwa, usiwe wa kimtu tena, apewe moyo wa kinyama, mpaka miaka saba ipite, akiwa hivyo. Kwa shauri la walinzi imekuja amri hii, yakafanyika kwa agizo lao watakatifu, kusudi walioko uzimani watambue kwamba: Yule Alioko huko juu ndiye autawalaye ufalme wa watu, naye humpa ampendaye, naye aliye mnyenyekevu kwa watu humwinua, aupate. Ndoto hii nimeiota mimi mfalme Nebukadinesari, nawe Beltesasari iseme maana yake, kwa kuwa wajuzi wote wa ufalme wangu hawakuweza kunijulisha maana yake lakini wewe utaweza, kwani roho ya miungu mitakatifu imo mwako. Kisha Danieli aliyeitwa jina lake Beltesasari akapigwa bumbuazi kitambo kidogo, mawazo yake yakamstusha; ndipo, mfalme alipomwambia Beltesasari kwamba: Ndoto na maana yake isikustushe! Beltesasari akamjibu akasema: Bwana wangu, ningependa, ndoto hii iwe yao wakuchukiao, nayo maana yake iwapate wakuinukiao! Umeona mti uliokuwa mkubwa na wenye nguvu, uliofika hata mbinguni kwa kilele chake, uliooneka katika nchi yote nzima; majani yake mazuri na matunda yake yakawa mengi, vyakula vilivyopatikana kwake vikawatoshea watu wote pia, chini yake kivulini wakapanga nyama wote wa porini, katika matawi yake wakakaa ndege wa angani. Wewe mfalme ndiwe mti huo, kwani u mkuu mwenye nguvu, ukuu wako umekua, ukafika hata mbinguni, ukatawala mpaka kwenye mapeo ya nchi. Tena mfalme ameona, mlinzi mtakatifu akishuka kutoka mbinguni, akasema: Ukateni mti huu na kuuangamiza! Lakini shina lenye mizizi yake liacheni mchangani, likiwa limefungwa kwa vyuma na kwa shaba katika mbuga yenye majani mabichi, liloweshwe na umande wa mbinguni, fungu lake liwe lao nyama wa porini, mpaka miaka saba ipite, akiwa hivyo. Hii ndiyo maana yake, mfalme: ni shauri lake Alioko huko juu, alilomkatia bwana wangu mfalme. Watakufukuza kwenye watu, ukae pamoja na nyama wa porini, tena watakulisha majani kama ng'ombe, nao umande wa mbinguni utakulowesha, miaka saba ipite, ukiwa hivyo, mpaka utakapotambua kwamba: Yule Alioko huko juu ndiye autawalaye ufalme wa watu, naye humpa ampendaye. Hapo wakisema, waliache shina lenye mizizi yake huo mti, ni kwamba: Ufalme wako utakurudia tena hapo, utakapojua, ya kuwa mbingu ndizo zitawalazo. Kwa hiyo, mfalme, shauri langu likupendeze: makosa yako yalipe kwa kutenda wongofu! Nayo maovu, uliyoyafanya, yalipe kwa kuwahurumia wanyonge! Hivyo utulivu wako utakuwa wa siku nyingi. Hayo yote yakampata mfalme Nebukadinesari. miezi kumi na miwili ilipopita, siku moja alipotembea huko Babeli jumbani mwake mwa kifalme juu, ndipo, mfalme aliposema kwamba: Kumbe huu sio mji mkubwa wa Babeli, nilioujenga mimi kuwa kao la kifalme kwa nguvu ya uwezo wangu, utukufu wangu utukuzwe! Neno hili lilipokuwa lingalimo kinywani mwa mfalme, sauti ikatoka mbinguni kwamba: Wewe mfalme Nebukadinesari, unapashwa habari, ya kuwa ufalme umekwisha kuondoka kwako. Watakufukuza kwenye watu, ukae pamoja na nyama wa porini, tena watakulisha majani kama ng'ombe; miaka saba itapita, ukiwa hivyo, mpaka utakapotambua kwamba: Yule Alioko huko juu ndiye autawalaye ufalme wa watu, naye humpa ampendaye. Papo hapo neno hilo likamtimilikia Nebukadinesari: akafukuzwa kwenye watu, akalishwa majani kama ng'ombe, mwili wake ukaloweshwa na umande wa mbinguni, mpaka nywele zake zikawa ndefu kama manyoya ya tai, nazo kucha zake zikawa ndefu kama za ndege. Siku hizo zilipopita, ndipo, mimi Nebukadinesari nilipoyaelekeza macho yangu mbinguni; ndipo, akili zangu ziliporudi kwangu, nikamtukuza yule Alioko huko juu, nikamsifu na kumheshimu aliye Mwenye uzima wa kale na kale, ukuu wake wa kutawala ni wa kale na kale, nao ufalme wake ni wa vizazi na vizazi. Wote wakaao nchini huwaziwa kuwa si kitu, yampendezayo huyafanya kwa vikosi vya mbinguni nako kwao wakaao nchini, tena hakuna awezaye kuuzuia mkono wake na kumwuliza: Unafanya nini? Papo hapo, akili zangu ziliporudi kwangu, nikapewa enzi yangu na utukufu wangu, ufalme wangu upate kutukuzwa. Wasemaji wangu wa shaurini na wakuu wangu wakanitafuta, nikarudishwa katika ufalme wangu, ukuu wangu ukaongezwa, ukazidi sana. Sasa mimi Nebukadinesari ninamsifu mfalme wa mbinguni na kumkuza na kumtukuza, kwani matendo yake yote ni ya kweli, njia zake ni za wongofu, nao waendeleao kujikuza anaweza kuwanyenyekeza. Mfalme Belsasari aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa, akanywa mvinyo mbele yao hao elfu. Belsasari alipokwisha kuonjaonja mvinyo akaagiza, wavilete vile vyombo vya dhahabu na vya fedha, baba yake Nebukadinesari alivyovichukua katika Jumba takatifu huko Yerusalemu, kwamba mfalme na wakuu wake na wakeze na masuria zake wanywee mumo humo. Kwa hiyo wakavileta vile vyombo vya dhahabu, walivyovichukua katika Jumba takatifu la Mungu huko Yerusalemu, mfalme na wakuu wake na wakeze na masuria zake wakanywea mumo humo. Walipokunywa mvinyo wakaisifu miungu ya dhahabu na ya fedha na ya shaba na ya chuma na ya miti na ya mawe. Mara vikatokea vidole vya mkono wa mtu, vikaandika mwangani pa taa penye chokaa ukutani mle jumbani mwa mfalme, mfalme akiuona mgongo wa mkono ulioandika. Ndipo, uso wake mfalme ulipokuwa mwingine, mawazo yake yakamstusha, maungo ya viuno vyake yakalegea, nayo magoti yake yakagonganagongana. Mfalme akalia kwa sauti kuu, wamletee waaguaji na Wakasidi na wachunguza nyota, kisha mfalme akawaambia hao wajuzi wa Babeli akisema: Mtu ye yote atakayeyasoma maandiko haya na kunieleza maana yake atavikwa nguo za kifalme, napo shingoni pake atapata mkufu wa dhahabu, naye atakuwa mwenye kutawala wa tatu katika ufalme. Basi, wakaingia wajuzi wote wa Babeli, lakini hawakuweza kuyasoma hayo maandiko wala kumjulisha mfalme maana yake. Ndipo, mfalme Belsasari alipozidi kustuka, nao uso wake ukawa mwingine kabisa, nao wakuu wake wakapotelewa na mizungu. Kwa ajili ya hayo maneno ya mfalme na ya wakuu wake mamake mfalme akaja mle chumbani, walimonywea, kisha mamake mfalme akasema kwamba: Wewe mfalme na uwe mwenye uzima kale na kale! Mawazo yako yasikustushe, wala uso wako usiwe mwingine! Katika ufalme wako yuko mtu mwenye roho ya miungu mitakatifu, hata siku za baba yako kwake yeye ulioneka mwangaza na utambuzi na ujuzi uliofanana na ujuzi wa miungu, baba yako Nebukadinesari akamweka kuwa mkuu wao waandishi na waaguaji na Wakasidi na wachunguza nyota, kweli baba yako mfalme aliyafanya. Kwani mwake imo roho kuu na akili na utambuzi wa kutambua maana ya ndoto na wa kufumbua mafumbo na wa kuvumbua njia zilizo ngumu za kuziona; roho hiyo imo mwake Danieli, mfalme aliyemwita jina lake Beltesasari. Basi, huyo Danieli na aitwe, yeye ataifumbua maana. Kisha Danieli akapelekwa mbele yake mfalme, mfalme akamwuliza Danieli akisema: Wewe ndiwe Danieli, mmoja wao Wayuda, baba yangu mfalme aliowateka na kuwahamisha kuja huku akiwatoa katika nchi ya Yuda? Nimesikia habari zako, ya kuwa roho ya miungu imo mwako, kwa hiyo mwako unaoneka mwangaza na utambuzi na ujuzi mwingi sana! Sasa hapa wajuzi na waaguaji wameletwa mbele yangu, wayasome maandiko haya, wanijulishe maana yake, lakini hawawezi kuifumbua maana yake hilo jambo. Lakini habari zako wewe nimesikia, ya kuwa unaweza kusema maana na kuyavumbua yaliyofunikwa; basi, kama unaweza kuyasoma maandiko haya na kunijulisha maana yao, utavikwa nguo za kifalme, napo shingoni pako utapata mkufu wa dhahabu, tena utakuwa mwenye kutawala wa tatu katika ufalme. Kisha Danieli akamjibu mfalme akisema: Kaa na vipaji vyako! Umpe mwingine matunzo yako! Lakini haya maandiko nitamsomea mfalme, nayo maana yao nitamjulisha. Wewe mfalme, Mungu Alioko huko juu alimpa baba yako Nebukadinesari ufalme na ukuu na enzi na utukufu. Kwa ajili ya ukuu, aliompa, watu wa makabila yote na wa koo zote, wao wote wenye ndimi za watu walitetemeka mbele yake kwa kumwogopa, kwani aliyetaka kumwua, akamwua; naye aliyetaka kumwacha, akamwacha kuwa mzima, naye aliyetaka kumkweza, akamkweza, naye aliyetaka kumnyenyekeza, akamnyenyekeza. Lakini moyo wake ulipojikuza, nayo roho yake ilipojisifu na kujivuna vibaya, ndipo, alipokumbwa katika kiti chake cha kifalme, wakamvua nao utukufu wake. Akafukuzwa kwenye watu, wakauwazia moyo wake kuwa kama wa nyama wa porini, akakaa pamoja na punda wa mwituni, wakamlisha majani kama ng'ombe, mwili wake ukaloweshwa na umande wa mbinguni, mpaka alipotambua, ya kuwa Mungu Alioko huko juu ndiye autawalaye ufalme wa watu, naye ampendaye humkweza, aupate. Nawe Belsasari u mwanawe, lakini hukuunyenyekeza moyo wako, ingawa uliyajua hayo yote. Ukamwinukia Bwana wa mbinguni, ukavitaka hivi vyombo vya Nyumba yake, wakutolee, wewe unywee mumo humo mvinyo pamoja na wake zako na masuria zako na wakuu wako, mkaisifu miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba na ya chuma na ya miti na ya mawe isiyoona, isiyosikia, isiyojua kitu; lakini hukumtukuza Mungu azishikaye pumzi zako mkononi mwake, naye ndiye azilinganyaye njia zako zote. Kwa hiyo ukatumwa naye huo mgongo wa mkono na haya maandiko yaliyoandikwa hapa. Nayo haya maandiko yaliyoandikwa hapa ni kwamba: Mene, Mene, Tekel, U-parsin Maana yao ni hii: Mene ni kwamba: Mungu amezihesabu siku za ufalme wako, akaukomesha Tekel ni kwamba: Umepimwa kwa mizani, ukaoneka kuwa mwepesi. Peresi ni kwamba: Ufalme wako umegawanyika, wakapewa Wamedi na Wapersia. Kisha Belsasari akatoa amri, wakamvika Danieli nguo za kifalme na mkufu wa dhahabu shingoni, wakatangaza, ya kuwa atakuwa mwenye kutawala wa tatu katika ufalme. Usiku uleule Belsasari, mfalme wa Wakasidi, akauawa. Ufalme wake akauchukua Mmedi Dario, naye alikuwa mwenye miaka kama 62. Kwa mapenzi yake Dario akaweka watawala nchi 120 wa kuuangalia ufalme, wakiwa po pote katika huo ufalme. Hao nao akawapatia wakuu watatu, mmoja wao akawa Danieli; wale watawala nchi hawakuwa na budi kuwatolea hawa hesabu, mfalme asipotelewe na mali. Ndipo, huyu Danieli alipowashinda wakuu wenziwe na watawala nchi, kwa kuwa Roho iliyo kuu ilikuwa mwake, naye mfalme akafikiri kumpa ufalme wote, auangalie. Kwa hiyo wakuu na watawala nchi wakatafuta jambo la kumwonea Danieli kwamba: anaukosea ufalme, lakini hawakupata jambo lo lote la kumwonea kwamba: amefanya vibaya, kwa kuwa alikuwa mwelekevu, halikuonekana kwake kosa lo lote wala tendo baya. Ndipo, hao waume waliposema: Kwake Danieli hatutapata jambo lo lote la kumwonea, tusipomwonea kwa hivyo, anavyomcha Mungu wake. Kisha wale wakuu na watawala nchi wakamwendea mfalme na kumpigia shangwe, wakamwambia: Mfalme Dario na uwe mwenye uzima kale na kale! Liwali wote wa ufalme na wakuu na wenye amri na wasemaji wa shaurini na watawala nchi wamepiga shauri pamoja kwamba: Itolewe amri ya mfalme na kutisha watu kwa ukali wa kwamba: Kila mtu atakayemwomba mungu wo wote au mtu muda wa siku thelathini, asikuombe wewe mfalme, atatupwa pangoni mwa simba. Sasa, mfalme, itoe amri hii ya huo mwiko, kaiandike kitabuni, isiwezekane kugeuzwa kwa hivyo, maongozi ya Wamedi na ya Wapersia yalivyo, wala isitanguliwe. Kwa sababu hiyo mfalme Dario akaiandika amri hiyo ya kutisha watu kwa ukali. Danieli aliposikia, ya kuwa hiyo amri imeandikwa, akaingia nyumbani mwake. Humo katika chumba cha juu yalikuwamo madirisha yaliyokuwa wazi kuuelekea Yerusalemu; ndimo, alimopigia magoti kila siku mara tatu akiomba na kumshukuru Mungu wake sawasawa, kama alivyovifanya siku za mbele. Kisha wale waume wakamwendea kwa kushangilia mioyoni, wakamwona Danieli, alivyomwomba Mungu wake na kumlalamikia. Kisha wakamkaribia mfalme, wakamwambia kwa ajili ya ile amri ya mfalme: Hukuandika amri ya kutisha watu kwamba: Kila mtu atakayemwomba mungu wo wote au mtu muda wa siku thelathini, asipokuomba wewe mfalme, atatupwa pangoni mwa simba? Mfalme akaitikia, akasema: Neno hili ni la kweli kabisa, haliwezekani kutanguliwa kwa hivyo, maongozi ya Wamedi na ya Wapersia yalivyo. Kisha wakamjibu mfalme na kumwambia: Danieli aliye mmoja wao Wayuda waliotekwa na kuhamishwa kuja huku, hakuchi, wala haishiki amri yako, mfalme, ya kutisha watu, uliyoiandika, ila huomba maombo yake kila siku mara tatu. Mfalme alipolisikia neno hili, halikumpendeza kabisa, akafikiri moyoni, jinsi atakavyomwokoa Danieli; mpaka jua likiingia, akawa akihangaikia mizungu ya kumponya. Ndipo, wale waume walipomwendea mfalme na kushangilia mioyoni, wakamwambia mfalme: Unajua, mfalme, ya kuwa kwa maongozi yetu Wamedi na Wapersia haiwezekani kugeuza katazo wala amri, mfalme aliyoitoa. Ndipo, mfalme alipoagiza, wamlete Danieli, wamtupe pangoni mwa simba. Naye akamwambia Danieli: Mungu wako, unayemtumikia pasipo kukoma, ndiye atakayekuokoa. Pakaletwa jiwe moja, likawekwa juu hapo pa kuliingilia lile pango, mfalme akalitia muhuri kwa pete yake yenye muhuri na kwa pete ya wakuu wake yenye muhuri, jambo la Danieli lisigeuzwe. Kisha mfalme akaenda jumbani mwake, akalala na kufunga mfungo, hata wakeze hakuwaingiza mwake, lakini usingizi hakuupata. Asubuhi mapema kulipopambazuka, mfalme akaondoka, akaenda na kulikimbilia lile pango la simba. Alipolifikia hilo pango karibu, akamwita Danieli na kupaza sauti kiwogawoga, yeye mfalme akasema na kumwuliza Danieli: Danieli uliye mtumishi wake Mungu aliye Mwenye uzima! Je? Mungu wako, unayemtumikia pasipo kukoma, ameweza kukuokoa katika simba? Ndipo, Danieli alipomjibu mfalme: Wewe mfalme, na uwe mwenye uzima kale na kale! Mungu ametuma malaika wake, akavifumba vinywa vya simba, hawakuniumiza, kwa kuwa mbele yake nimeonekana kuwa mtu asiyekosa; hata mbele yako, mfalme, hakuna kiovu, nilichokifanya. Ndipo, mfalme alipomfurahia sanasana, akaagiza kumtoa Danieli pangoni; basi, Danieli alipokwisha kutolewa mle pangoni hamkuonekana mwilini mwake kidonda cho chote, kwani alimtumaini Mungu wake. Kisha mfalme akaagiza kuwaleta wale waume waliomchongea Danieli, wawatupe humo pangoni mwa simba, wao na wana wao na wake zao. Walipokuwa hawajafika pangoni chini, simba wakawakamata, wakawavunja mifupa yao yote. Kisha mfalme Dario akawaandikia watu wa makabila yote na wa koo zote, wao wote wenye ndimi za watu waliokaa katika nchi yote nzima, kwamba: Utengemano wenu na uwe mwingi! Kwangu inatoka amri hii: Katika ufalme wangu wote, ninaoutawala, watu sharti watetemeke mbele yake Mungu wa Danieli kwa kumwogopa. Kwani yeye ndiye Mungu Mwenye uzima akaaye kale na kale, ufalame wake hauangamii, kutawala kwake hakuna mwisho. Yeye huokoa na kuponya, hufanya vielekezo na vioja mbinguni na nchini, naye ndiye aliyemwokoa Danieli mikononi mwa simba. Kisha Danieli akapata kutulia siku za ufalme wa Dario, hata siku za ufalme wa Kiro aliyekuwa Mpersia. Katika mwaka wa kwanza wa mfalme Belsasari, mfalme wa Babeli, Danieli aliota ndoto, akaona maono kwa macho yake alipolala kitandani. Kisha akaiandika hiyo ndoto na kuyasema mambo yake makuu. Basi, Danieli akayasimulia kwamba: Katika ndoto ya usiku nilikuwa nikitazama, mara nikaziona pepo nne za mbinguni zilivyoitokea Bahari Kubwa kwa nguvu. Ndipo, nyama wakubwa wanne walipotoka baharini, kila mmoja wao alikuwa wa namna yake. Wa kwanza alikuwa kama simba, lakini alikuwa na mabawa ya tai, nikamtazama, mpaka mabawa yake yakinyonyolewa manyoya, akachukuliwa nchini, akasimamishwa kwa miguu miwili kama mtu, akapewa hata moyo wa kimtu. Mara nikaona nyama mwingine, ndio wa pili, alifanana na nyegere, alisimama upande mmoja tu, namo kinywani mwake alishika mbavu tatu kwa meno yake, akaambiwa: Inuka, ule nyama nyingi! Baadaye nilipotazama tena, nikaona nyama mwingine aliyekuwa kama chui, lakini mgongoni mwake alikuwa na mabawa manne ya ndege, navyo vichwa vyake huyu nyama vilikuwa vinne, akapewa kutawala. Baadaye nilipotazama tena katika hayo maono ya usiku, mara nikaona nyama wa nne, akastusha na kutia woga kwa kuwa na nguvu kabisa; alikuwa na meno makubwa ya chuma, akala na kuvunjavunja, nayo yaliyosalia akayakanyagakanyaga kwa miguu yake, alikuwa mwingine kabisa, hakufanana nao nyama wa kwanza, tena alikuwa na pembe kumi. Nilipoziangalia hizo pembe, mara nikaona pembe nyingine ndogo iliyotokea katikati yao, nazo hizo pembe za kwanza kwao zikang'olewa tatu mbele yake hiyo, tena pembe hiyo ilikuwa yenye macho kama macho ya mtu na yenye kinywa kilichosema makuu. Nilipokuwa nikimtazama, vikaletwa viti vya kifalme; kisha mtu mwenye siku nyingi akaja kukaa, alikuwa amevaa nguo nyeupe zing'aazo kama chokaa juani, nazo nywele za kichwani pake zilikuwa kama manyoya ya kondoo yaliyotakata sana, kiti chake cha kifalme kilikuwa cha miali ya moto, nayo magurudumu ya kiti chake yalikuwa ya moto uwakao. Mto wa moto ukaja, ukaijiendea na kutoka mbele yake; maelfu na maelfu wakamtumikia, milioni na milioni wakasimama mbele yake, wenye hukumu wakakaa, kisha vitabu vikafunuliwa. Nikawa nikitazama hapohapo kwa ajili ya makelele makubwa, ambayo iliyapiga ile pembe isemayo; nikatazama vivyo hivyo, mpaka yule nyama akiuawa, mwili wake ukaangamizwa ukitupwa motoni, uteketezwe. Kisha nao wale nyama wengine walinyang'anywa nguvu zao za kutawala, kwani walikuwa wamekatiwa wingi wa siku zao za kuwapo, wasipite wala mwaka wala siku. Nilipokuwa nikitazama katika hayo maono ya usiku mara nikaona, alivyokuja akichukuliwa na mawingu ya mbinguni aliyekuwa kama mwana wa mtu, akafika kwake yule mwenye siku nyingi, wakimpeleka kuja mbele yake. Akapewa nguvu za kutawala na macheo na ufalme, watu wa makabila yote na wa koo zote, wao wote wenye ndimi za watu wamtumikie, nguvu zake za kutawala ni za kale na kale, hazina mwisho, hata ufalme wake hautaangamia. Roho yangu mimi Danieli ikaumia mwilini mwangu, nayo maono ya macho yangu yakanitia woga. Nikamkaribia mmoja wao waliosimama hapo, nikamwomba kuniambia maana ya kweli ya hayo yote; akanijibu na kunifumbulia hayo mambo kwamba: Nyama wale wakubwa mno walio wanne ndio wafalme wanne watakaoinuka katika nchi. Kisha watakatifu wake Alioko huko juu watapata ufalme, nao wataushika ufalme kale na kale, kweli siku zitakazokuja zote za kale na kale. Nikamwuliza tena maana ya kweli ya nyama wa nne aliyekuwa mwingine kabisa, asifanane na wenzake wote, aliyestusha kabisa kwa kuwa mwenye meno ya chuma na mwenye kucha za shaba, aliyekula na kuvunjavunja, nayo yaliyosalia aliyakanyagakanyaga kwa miguu yake. Nikauliza nayo maana ya zile pembe kumi za kichwani pake, nayo maana ya ile pembe nyingine, ambayo mbele yake zikang'oka pembe tatu, iliyokuwa yenye macho kama ya mtu, tena yenye kinywa kilichosema makuu; naye alionekana kuwa mkubwa kuliko wenziwe. Nami nilikuwa nimeona, pembe hiyo ilivyofanya vita na watakatifu na kuwashinda, mpaka yule mwenye siku nyingi alipokuja; ndipo, watakatifu wake Alioko huko juu walipopewa kuhukumu, ndipo, siku zao watakatifu zilipotimia za kuushika ufalme. Akaniambia haya: Huyo nyama wa nne ndio ufalme wa nne utakaokuwa katika nchi, nao utakuwa mwingine, usifanane na ufalme wote, utaila nchi yote nzima, utaiponda kwa kuikanyagakanyaga. Nazo zile pembe kumi ni kwamba: Katika ufalme huo watainuka wafalme kumi; nyuma yao atainuka mwingine asiyefanana na wenzake waliokuwa mbele yake, naye ataangusha chini wafalme watatu. Tena atasema maneno ya kumbeza Alioko huko juu, nao watakatifu wake Alioko huko juu atawapondaponda; tena atajipa moyo wa kuzigauza sikukuu, atoe nyingine, hata maongozi, atoe mengine. Nao watakatifu watatiwa mikononi mwake kipande cha siku na vipande viwili vya siku na nusu ya kipande cha siku. Zitakapokwisha atahukumiwa, wamnyang'anye nguvu zake za kutawala, wazitoweshe na kumwangamiza kabisa. Ndipo, ufalme na nguvu za kutawala na ukuu wa ufalme wote ulioko chini ya mbingu utakapopewa ukoo wa watakatifu wake Alioko huko juu, ufalme wake ni wa kale na kale, nazo nguvu zote zitawalazo zitamtumikia na kumtii. Huu ndio mwisho wa hilo jambo. Mimi Danieli mawazo yangu yakanitisha sana, nao uso wangu ukawa mwingine, nikaliweka jambo hilo moyoni mwangu. Katika mwaka wa tatu wa mfalme Belsasari mimi Danieli nikatokewa na ndoto, ile ya kwanza ilipokwisha kunitokea. Yako, niliyoyaona katika hiyo ndoto; napo hapo, nilipoyaona, nilikuwa katika mji wa kifalme wa Susani ulioko katika jimbo la Elamu. Nami nilipoyaona katika hiyo ndoto nilikuwa kwenye mto wa Ulai. Nilipoyainua macho yangu, nitazame, mara nikaona dume moja la kondoo aliyesimama hapo penye mto, naye alikuwa na pembe mbili, nazo hizo pembe zilikuwa ndefu, tena moja ilikuwa ndefu kuliko ya pili, nayo hiyo ndefu ndiyo iliyotokea mwisho. Nikamwona huyo dume la kondoo, alivyorukia upande wa baharini na wa kaskazini na wa kusini, tena hakuwako nyama yeyote aliyeweza kusimama mbele yake, wala hakuwako aliyeweza kuokoa mkononi mwake, akafanya yaliyompendeza kwa kujikuza. Nilipokuwa sijamtambua vema, mara nikaona dume la mbuzi aliyetoka machweoni kwa jua, akapita juu ya nchi yote nzima pasipo kugusa mchanga wa chini kwa miguu; huyo dume la mbuzi alikuwa na pembe kubwa mno katikati ya macho yake. Akamjia yule dume la kondoo, mwenye pembe mbili, niliyemwona, akisimama penye mto, akamkimbilia kwa makali ya nguvu zake. Nikamwona, alivyomfikia yule dume la kondoo, akamrukia kwa ukali mwenye uchungu, akampiga yule dume la kondoo, akazivunja pembe zake mbili, naye dume la kondoo hakuwa na nguvu ya kusimama mbele yake, kwa hiyo akambwaga chini, akamkanyagakanyaga, tena hakuwako aliyemwokoa yule dume la kondoo mkononi mwake. Kisha dume la mbuzi akajikuza kabisa; nguvu zake zilipozidi, ndipo, pembe yake kubwa ilipovunjika, mahali pake pakatokea nyingine nne kubwa mno, zikazielekea pande nne za upepo wa mbinguni. Kwao hizo katika moja ikatoka pembe moja ndogo, ikakua sanasana, ikaelekea upande wa kusini na wa maawioni kwa jua na wa ile nchi yenye utukufu. Ikakua kufika kwenye kikosi cha mbinguni, vinginevyo vya hicho kikosi ikavibwaga chini nazo nyota mojamoja, ikaziponda kwa kuzikanyagakanyaga. Kisha ikajikuza, imshinde naye Mkuu wa hicho kikosi, kwa hiyo akanyimwa matambiko yake ya kila siku, nalo Kao lake takatifu likaachwa. Nacho hicho kikosi kikatolewa pamoja na yale matambiko kwa kupotolewa; nayo mambo ya kweli ikayatupa chini, hivyo yakaendelea iliyoyafanya. Ndipo, niliposikia, mtakatifu mmoja akisema: mtakatifu mwingine akamwuliza yuyo huyo aliyesema: Mambo ya hili ono yatakuwa mpaka lini? Hayo ya matambiko ya kila siku na ya mapotovu yanayoangamiza? Nayo yale ya kukitoa Kikao kitakatifu nacho kikosi, vikanyagwekanyagwe? Akaniambia: Mpaka zipite 2300 za kuchwa na kucha; ndipo, Patakatifu patakapoyapata yapapasayo. Mimi Danieli nilipoiona ndoto hii nikatafuta njia ya kuitambua. Mara nikaona aliyesimama mbele yangu mwenye mwili wa kimtu. Nikasikia sauti ya mtu iliyotoka katika mto wa Ulai, ikaita kwamba: Gaburieli, mtambulishe mtu huyu aliyoyaona! Akaja huko, nilikosimama; lakini alipokuja, nikastuka, nikaanguka kifudifudi, akaniambia: Tambua, mwana wa mtu, ya kuwa hilo ono linaonyesha yatakayokuwa siku za mwisho! Aliposema nami, nikashikwa na usingizi kabisa, nao uso wangu ukaelekea chini, akanigusa, akanisimamisha tena hapo, nilipokuwa nimesimama, akasema: Tazama, mimi nitakujulisha yatakayokuwa penye mwisho wa makali haya, kwani hayo yanayaelekea yale ya mwisho. Dume la kondoo, uliyemwona mwenye pembe mbili, ndio wafalme wa Wamedi na wa Wapersia. Naye dume la mbuzi mwenye manyoya mengi ni mfalme wa Wagriki, nayo ile pembe kubwa iliyokuwa katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza. Tena ikivunjika, mahali pake zikitoka nyingine nne, ni kwamba: Nchi za kifalme nne zitatoka katika taifa lake, lakini hazitakuwa na nguvu yake yeye. Penye mwisho wa ufalme wao, wapotovu watakapoyatimiza mapotovu yao, patainuka mfalme mwenye uso mkali atambuaye mizungu mibaya. Nguvu zake zitazidi, lakini si kwa nguvu zake yeye; atafanya vioja vibaya vya kuangamiza, tena atakapovifanya atafanikiwa, awaangamize wenye nguvu nao ukoo wao watakatifu. Kwa werevu wake atayaendesha madanganyo yaliyomo mkononi mwake, atajikuza moyoni mwake, aangamize wengi kwa kuwajia kwa upole. Lakini atakaposimama, ampingie naye aliye Mkuu wa wakuu, ndipo, atakapovunjwa pasipo kukamatwa kwa mikono Nayo, uliyoyaona ya kuchwa na kucha na kuambiwa habari zao, ni ya kweli. Lakini wewe iandike ndoto hii, kisha iweke kifichoni, kwani ni ya mambo ya siku nyingi. Kisha mimi Danieli nikazimia, nikawa mgonjwa siku hizo; kisha nikaondoka kitandani, nikafanya kazi ya kumtumikia mfalame. Lakini nikahangaika sana kwa ajili yao hayo, niliyoyaona, lakini hakuwako aliyenitambua. Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahaswerosi, aliyekuwa wa kizazi cha Wamedi, aliyepata kuwa mfalme wa ufalme wa Wakasidi, basi, katika mwaka wa kwanza wa ufalme wake, mimi Danieli niliiangalia hesabu ya miaka katika vitabu, ambayo Neno lake Bwana lilimwambia mfumbuaji Yeremia, ya kuwa miaka 70 itamalizika, Yerusalemu ikikaa kuwa mabomoko. Ndipo, nilipouelekeza uso wangu kwake Bwana Mungu, nipate kumwomba na kumlalamikia nikifunga mfungo na kuvaa gunia na kukaa majivuni. Nikamwomba Bwana Mungu wangu nikiungana na kusema hivyo: E Bwana, ndiwe Mungu mkuu aogopeshaye, unalishika agano la kuwahurumia wakupendao na kuyashika maagizo yako. Tumekosa na kukora manza, tukaacha kukucha na kukutii, tukaondoka kwenye maagizo yako na maongoi yako. Hatukuwasikia watumishi wako wafumbuaji waliosema kwa Jina lako kwa wafalme wetu na kwa wakuu wetu na kwa baba zetu na kwa watu wa ukoo wote wa nchi hiyo. Wewe Bwana u mwenye wongofu, lakini sisi nyuso zinatuiva kwa soni; ndivyo, vinavyojulika leo: sisi waume wa Yuda nao wakaao Yerusalemu nao Waisiraeli wote walioko karibu nao walioko mbali katika nchi zote, ulikowatawanyia kwa ajili ya matendo yao, waliyokutendea, Bwana, nyuso zinatuiva kwa soni sisi na wafalme wetu na wakuu wetu na baba zetu, kwa kuwa tumekukosea wewe. Lakini kwake Bwana Mungu wetu ziko huruma, atuondolee makosa, ijapo tuwe tumekataa kumtii. Hatukuisikia sauti ya Bwana Mungu wetu, tuyafuate Maonyo yake, aliyotupa mikononi mwa watumishi wake wafumbuaji, tuyaangalie. Waisiraeli wote wakapita tu penye Maonyo yako, wakaenda zao pasipo kuisikia sauti yako; kwa sababu hiyo tukamwagiwa kiapizo, kikatupata nacho kiapo kilichoandikwa katika Maonyo ya Mose, mtumwa wake Mungu, kwani tulimkosea. Akayatimiza maneno yake, aliyoyasema ya kututisha sisi na waamuzi wetu waliotuamua ya kwamba: Atatuletea kibaya kikubwa kisichofanyika po pote chini ya mbingu, kama kitakavyofanyika Yerusalemu. Vikawa, kama vilivyoandikwa katika Maonyo ya Mose; hicho kibaya chote kikatujia, lakini sisi hatukujipendekeza usoni pa Bwana Mungu wetu tukiyaacha maovu, tuliyoyafanya, tujipatie kwako utambuzi wa kweli. Kwa hiyo Bwana akakiangalia hicho kibaya, akifikishe kwetu, kwani Bwana Mungu wetu ni mwongofu, ayanyoshe matendo yake yote, anayoyatenda. Lakini hatukuisikia sauti yake. *Lakini na sasa ndiwe Bwana Mungu wetu! Uliwatoa walio ukoo wako katika nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu ukajipatia Jina, kama inavyojulika leo; nasi tukakukosea, tukaacha kukucha. Bwana, kwa ajili ya wongofu wako wote nakuomba: Makali yako yenye moto na yarudi nyuma, yauache mji wako wa Yerusalemu, mlima wako mtakatifu ulimo! Kwani kwa ajili ya makosa yetu na kwa ajili ya manza, baba zetu walizozikora, Yerusalemu pamoja na ukoo wako umegeuka kuwa wa kutukanwa tu kwao wote waliokaa na kutuzunguka. Sasa Mungu wetu, yasikie maombo ya mtumwa wako na malalamiko yake! Uangaze uso wako juu ya Patakatifu pako palipobomolewa, kwa kuwa ndiwe Bwana! Mungu wangu, litege sikio lako, usikie! Yafumbue macho yako, uyaone mabomoko yetu, nao mji huo ulioitwa kwa Jina lako! Kwani tukiyatoa haya malalamiko yetu usoni pako, si kwa wongofu wetu sisi, ila kwa huruma zako nyingi.* Sikia, e Bwana! Tuondolee makosa, e Bwana! Sikiliza, e Bwana! Yafanye pasipo kukawia kwa ajili yako, Mungu wangu! Kwani mji wako nao ukoo wako umeitwa kwa Jina lako! Nilipokuwa ninasema bado nikiomba na kuyaungama makosa yangu na makosa yao walio ukoo wangu wa Isiraeli na kuyatoa malalamiko yangu usoni pa Bwana Mungu wangu kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu, nilipokuwa ninasema bado na kuyaomba hayo, mara yule mtume Gaburieli, niliyemwona katika ndoto ya kwanza, akaja akiruka upesi, akanigusa saa ile, walipotolea tambiko la jioni. Akanifundisha akisema na mimi kwamba: Danieli, sasa nimetokea kukupatia akili zenye utambuzi. Ulipoanza kulalamika, ndipo, palipotolewa neno, nami nimekuja, niliseme kwako, kwani ndiwe mtu wa kupendezwa naye; sasa liangalie hilo neno, upate kulitlambua nalo lile ono! Majuma 70 ndiyo, waliyokatiwa walio ukoo wako na wa mji wako mtakatifu ya kuyalipa mapotovu na kuyakomesha makosa na kuzifunika manza, walizozikora, na kuleta wongofu wa kale na kale na kuyatia muhuri maono ya wafumbuaji na kupaeua Patakatifu Penyewe. Ujue na kuvitambua vema: Tangu hapo lilipotoka lile neno la kuujenga Yerusalemu tena, mpaka kutokea kwake mkuu aliyepakwa mafuta ni majuma 7, tena majuma 62 utajengwa tena viwanja na boma, lakini siku zile zitakuwa za kusongwa. Hayo majuma 62 yatakapokwisha, ndipo, yeye aliyepakwa mafuta atakapoangamizwa, naye atakuwa hanalo kosa lo lote. Kisha watu wa mkuu atakayekuja wataubomoa huo mji napo Patakatifu, nao mwisho wake utakuwa wa kufurikiwa na maji, tena mpaka mwisho yatakuwa mapigano na maangamizo, waliyotakiwa kale. Naye atafanyia wengi agano lenye nguvu la juma 1, kisha hilo juma litakapofika kati, atawakomesha watu, wasitoe wala ng'ombe wala vilaji vya tambiko, napo pembeni pa kutambikia atasimama mwangamizaji atapishaye, mpaka yatimie na kumfurikia yeye mwangamizaji, aliyotakiwa kale. Katika mwaka wa tatu wa Kiro, mfalme wa Wapersia, Danieli aliyeitwa jina lake Beltesasari akafunuliwa neno; hilo neno ni la kweli, masumbufu yatakuwa makubwa. Naye akalitambua hilo neno, akayatambua nayo, aliyoyaona. Siku zile mimi Danieli nilikuwa nikikaa matanga siku za majuma matatu. Sikula chakula kilichopendeza, wala nyama, wala mvinyo haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta, mpaka siku za majuma matatua ziishe. Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza mimi Danieli nilikuwa penye ukingo wa jito kubwa, nalo ndilo Hidekeli. Nilipoyainua macho yangu na kutazama, mara nikaona mwanamume mmoja aliyevaa nguo nyeupe ya ukonge, namo viunoni pake alikuwa amefunga mshipi wa dhahabu ya Ufazi. Mwili wake ulikuwa kama kito cha Tarsisi, uso wake ulionekana kuwa kama umeme, nayo macho yake yalikuwa kama mienge ya moto, mikono yake na miguu yake ilimerimeta kama shaba iliyokatuliwa, sauti ya kusema kwake ikawa kama uvumi wa watu wengi. Mimi Danieli nikayaona peke yangu hayo yaliyooneka hapo, lakini mwenzangu waliokuwa nami hawakuyaona hayo kwa kupigwa na bumbuazi kabisa; ndipo, walipokimbia, wajifiche. Mimi nikasalia peke yangu, nami nilipoyaona hayo makuu, yalivyooneka, haikusalia nguvu mwangu, nayo yaliyokuwa mazuri kwangu yakageuka kuwa mabaya, nguvu zangu zikanipotea kabisa. Nikasika sauti ya maneno yake, tena papo hapo, nilipoisikia sauti ya maneno yake, nikashikwa na usingizi kabisa, nikaanguka kifudifudi, uso wangu ukaelekea chini. Mara mkono ukanigusa, ukanisaidia kuinuka, kwa kuwa magoti na viganja vya mikono vilikuwa vikitetemeka. Kisha akaniambia: Danieli, ndiwe mtu wa kupendezwa naye; yatambue hayo maneno, mimi nitakayokuambia, ukisimama hapohapo, unaposimama! kwani nimetumwa kwako. Aliponiambia neno hili, nikainuka na kutetemeka. Akaniambia: Usiogope, Danieli! Kwani tangu siku ya kwanza, ulipojipa moyo wa kutaka utambuzi kwa kujinyenyekeza mbele ya Mungu wako, maneno yako yamesikiwa, nami nimekuja kwa hayo maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Persia akasimama mbele yangu na kunipingia siku ishirini na moja; mara Mikaeli aliye miongoni mwao wakuu wenyewe akaja kunisaidia, nilipokuwa nimeachwa peke yangu kushindana nao wafalme wa Persia. Sasa nimekuja, nikutambulishe, yatakayowapata walio ukoo wako siku za mwisho; kwani ono hili ni la siku zisizotimia bado. Aliponiambia maneno haya, nikauelekeza uso wangu chini, maana sikuweza kusema. Mara yeye aliyefanana na wana wa watu akaigusa midomo yangu na kukifumbua kinywa changu; ndipo, nilipoweza kusema tena, nikamwambia aliyesimama mbele yangu: Bwana wangu, kwa hayo niliyoyaona, mastusho yakaniguia, nikageuka, nguvu zangu zikanipotea kabisa. Mimi niliye mtumwa wa Bwana wangu nitawezaje kusema na wewe uliye Bwana wangu? Kwani kwangu mimi hakuna nguvu zilizoko bado, wala pumzi haikusalia mwangu. Ndipo, yeye aliyefanana na mtu aliponigusa tena, akanitia nguvu, akaniambia: Usiogope! Ndiwe mtu wa kupendezwa naye; tulia tu na kujipa moyo, nguvu zikurudie! Aliponiambia haya, ndipo, nilipopata nguvu, nikamwambia: Bwana wangu na aseme! Kwani umenitia nguvu. Akauliza: Unajua, kama ni kwa sababu gani, nikikujia? Sasa nitarudi kupigana naye mkuu wa Persia. Hapo, nitakapotoka kwake, papo hapo atakuja mkuu wa Ugriki. Lakini kwanza nitakueleza yaliyoandikwa katika kitabu cha kweli. Hakuna hata mmoja ajipaye moyo wa kunisaidia kupigana nao hao, ila mkuu wenu Mikaeli. Lakini nami nalisimama upande wake katika mwaka wa kwanza wa Mmedi Dario, nikamsaidia kwa kumtia nguvu. Sasa nitakuonyesha yatakayokuwa kweli: Tazama, watandokea bado wafalme watatu wa Persia, wa nne atakuwa mwenye mali nyingi sana kuliko wote; kwa hizo nguvu zake, atakazozipata kwa mali zake nyingi, atawainua wote kuuendea ufalme wa Ugriki. Kisha ataondokea mfalme mwenye nguvu za kupiga vita, naye atatawala kwa uwezo mwingi, atafanya yatakayompendeza. Lakini hapo, atakapokwisha kuondokea, ufalme wake utavunjika, ukatwe vipande kwenye pepo zote nne za mbinguni; lakini hautakuwa wao walio uzao wake, wala hapatakuwa atakayetawala, kama yeye alivyotawala, kwani ufalme wake utang'olewa, uwe wa wengine, wale wasiupate. Kisha mfalme wa kusini atapata nguvu, lakini mmoja wa wakuu wake atapata nguvu kumshinda mwenyewe, kisha atatawala kwa uwezo, nao ufalme wake utakuwa mkubwa. Miaka itakapopita, watafanya mapatano, naye binti mfalme wa kusini atakwenda kwake mfalme wa kaskazini kutengeneza matengenezo, lakini naye yule binti mfalme nguvu za mkono wake zitampotea, yule mfalme asikae na nguvu za mkono; ndipo, yule binti mfalme atakapotolewa pamoja nao waliompeleka na mzazi wake naye aliyemtia nguvu siku zile. Kisha pataondokea mahali pake chipukizi la shina lake; yeye atamwendea mwenye vile vikosi, aingie bomani mwa mfalme wa kaskazini na kumfanyizia vita, nazo nguvu zake zitamshinda yule. Ndipo, atakapoichukua miungu yao na vinyago vyao na vyombo vyao viwapendezavyo vya fedha na vya dhahabu, ataviteka na kuvipeleka Misri, kisha atakaa miaka na miaka, asimwendee tena mfalme wa kaskazini. Lakini yule atakuja, auingie ufalme wa mfalme wa kusini, kisha atarudi katika nchi yake. Lakini wanawe watatengeneza vita wakikusanya vikosi vingi mno vivumavyo; kisha mmoja atakwenda kuifurikia na kuieneza hiyo nchi, katika safari ya pili atapeleka vita mpaka bomani kwake. Ndipo, mfalme wa kusini atakapochafuka kwa uchungu, atoke kupigana naye mfalme wa kaskazini; yule ataleta vikosi vingi, lakini vitatiwa mkononi mwake huyu; ndipo, vitakapochukuliwa, ingawa viwe vingi. Naye moyo wake utajikuza, lakini hatashinda kabisa, ijapo aangushe maelfu na maelfu. Mfalme wa kaskazini atarudi na kuleta vikosi vilivyo vingi kuliko vile vya kwanza. Siku nyingi na miaka itakapopita, atakuja navyo hivyo vikosi vikubwa vyenye mata mengi. Siku hizo wengi watamwinukia mfalme wa kusini, hata wana wao walio ukoo wako wenye ukorofi watainuka, wayatimize mambo uliyoyaona, lakini watajikwaa, waanguke. Ndipo, mfalme wa kaskazini atakapokuja, atamzungushia ukingo wa mchanga, auteke mji wake ulio na boma. Ndipo, itakapokuwa, mikono yao wakusini isishupae, hata mafundi wake wa vita wasiwe na nguvu za kusimama. Naye yeye amjiaye atafanya, kama anavyopendezwa, kwani hatakuwako atakayesimama mbele yake. Hata katika nchi hiyo yenye utukufu atakaa, mikono yake ikiiangamiza. Kisha atauelekeza uso wake kuja huko na enzi yote ya ufalme wake, afanye mapatano naye akimpa mwanawe, awe mkewe, aiangamize nchi hiyo, lakini jambo hili halitakuwa, hatafanikiwa. Kisha atauelekeza uso wake kwenda kupiga vita katika nchi za baharini, nazo nyingi ataziteka. Lakini huko kutakuwa na mpiga vita atakayeyakomesha matusi yake, asitukane tena, akimlipisha hayo matusi. Kisha atauelekeza uso wake kwenda kuiteka miji yenye maboma katika nchi yake; ndipo, atakapojikwaa na kuanguka, asionekane tena. Mahali pake ataondokea mwingine atakayetuma mtoza kodi penye utukufu wa ufalme wake; lakini kwa muda wa siku chache atavunjwa, lakini haitakuwa kwa ukali wa mtu wala kwa mapigano. Mahali pake ataondokea mtu abezwaye, wasiyempa macheo ya ufalme; naye atauingia kwa kuja kwa upole, aushike ufalme kwa kujitendekeza na kusema maneno matamu. Kisha wale wenye mikono ya nguvu waliokuja kumfurikia watafurikiwa naye na kuvunjwa, vilevile naye mkuu aliyefanya maagano naye. Papo hapo atakapokwisha kufanya urafiki naye, atamdanganya akimjia na kumshinda, ijapo awe na watu wachache tu. Kwa upole ataziingia nchi zenye manono, afanye mambo, wasiyoyafanya baba zake wala baba za baba zake, akitapanya kwao mapokonyo na mateka na mali zo zote, miji yenye maboma akiiwazia mizungu ya kuipata, lakini vitakuwa siku hizo tu zilizokatwa. Kisha ataviinua vikosi vyake kwa kujipa moyo wa kumwendea mfalme wa kusini kwa hizo nguvu kuu za vikosi vyake. Naye mfalme wa kusini atatengeneza vita na kuvipanga vikosi vyake vikubwa vilivyo vyenye nguvu kabisa, lakini hatashinda; kwani watakaomwazia mawazo ya njama ndio wanaokula naye vilaji vyake vya urembo; wao ndio watakaomvunja, vikosi vyake navyo vitatawanyika po pote, wengi wao watakufa kwa kuumizwa. Kisha hao wafalme wawili wataielekeza mioyo yao kufanyiana mabaya, wataambiana maneno ya uwongo wakikaa mezani pamoja, lakini hawatafanikiwa, kwani mwisho utakuja siku zilezile zilizokwisha kukatwa. Kisha atarudi katika nchi yake na kuchukua mali nyingi, lakini moyo wake utataka kulitengua Agano takatifu, naye atafanya, kisha atarudi katika nchi yake. Siku zilizokatwa zitakapotimia, atairudia nchi ya kusini, lakini safari hii ya pili haitakuwa, kama ya kwanza ilivyokuwa. Kwani merikebu za Wakiti zitamjia; ndipo, moyo utakapompotea. Basi, atarudi, alitolee Agano takatifu makali yake, kisha atarudi akiwatazamia walioliacha hilo Agano takatifu. Kisha mikono yao, aliowaweka huko, itapachafua Patakatifu palipokuwa boma la nguvu, watayakomesha matambiko ya kila siku, kisha wataweka hapo mwangamizaji atapishaye. Nao walioacha kulicha lile Agano atawashurutisha kwa maneno madanganyifu, wamwache naye Mungu, lakini hao wamjuao Mungu wao watajipatia nguvu za kufanya yawapasayo. Kisha hao wenye ujuzi huo watatambulisha wengine wengi, ijapo waumizwe vibaya siku nyingi kwa panga na kwa mioto na kwa mafungo ya kuhamishwa na kwa kunyang'anywa. Watakapoumizwa hivyo watasaidiwa kidogo tu, kwani wengi wataandamana nao kwa kujitendekeza tu. Namo miongoni mwao hao wenye ujuzi wengine watajikwaa, wapate kuyeyushwa, kusudi watakaswe na kueuliwa, mpaka siku za mwisho zitakapotimia, nao utakuja siku zilezile zilizokwisha kukatwa. Mfalme yule atafanya, kama anavyopendezwa, atajivuna na kujiwazia kuwa mkuu kuliko mungu wo wote, aseme maneno ya kustaajabisha kwa kumbeza naye Mungu aishindaye miungu; naye atayaendesha mambo hayo, mpaka siku za makali zitakapotimia, k kwani aliyotakiwa hayana budi kufanyika. Nayo miungu ya baba zake haiangalii, wala mungu wa kike upendezao wanawake, wala mungu wo wote mwingine hamwangalii, kwani anajiwazia kuwa mkuu kuliko yote. Mahali pao atamheshimu mungu wa maboma nao mungu, baba zake wasiyemjua, atamheshimu kwa kumtolea dhahabu na fedha na vito na vitu vingine vipendezavyo. Katika miji yenye maboma atafanya hivyo kwa ajili ya huyo mungu mgeni: atakayemwungama atampa macheo mengi, tena atampa watu wengi kuwatawala, nayo nchi atamgawia kuwa malipo yake. Siku za mwisho mfalme wa kusini atapigana naye; ndipo, naye mfalme wa kaskazini atakapomkimbilia kama upepo wa kimbunga kwa magari pamoja na wapanda farasi na kwa merikebu nyingi, aziingie hizo nchi na kuzifurikia na kuzieneza. Kisha ataiingia nayo hiyo nchi yenye utukufu; ndipo, nchi nyingi zitakapoangamizwa; zitakazopona mikoni mwake ni za Edomu na za Moabu na wakuu wao wana wa Amoni. Kisha ataukunjua mkono wake, aziteke hizo nchi; hapo nchi ya Misri nayo haitapata kupona. Namo mikononi mwake mwenye nguvu vitakuwamo vilimbiko vya dhahabu na vya fedha na vyombo vyote vya Misri vipendezavyo; kwa hiyo nao Walibia na Wanubi watamfuata. Lakini habari zitokazo upande wa maawioni kwa jua na wa kaskazini zitamstusha; ndipo, atakapoondoka kwa makali makubwa yenye moto, aje kuangamiza na kutowesha wengi. Atalipiga hema lake la kifalme katikati ya bahari na ya mlima wenye utukufu na utakatifu; ndipo, mwisho wake utakapokuja, lakini hatakuwako atakayemsaidia. Siku zile atatokea Mikaeli aliye mkuu mwenyewe anayewasimimia wana wao walio ukoo wako, kwa maana zitakuwa siku za maumivu yasiyokuwa bado tangu mwanzo wa kuwapo kwa watu, wala hayatakuwa mpaka siku zile. Lakini walio ukoo wako watapona, ni wao wote watakaoonekana, ya kuwa wameandikwa katika kile kitabu. Nao wengi walalao ndani ya nchi uvumbini wataamka, wengine kupata uzima wa kale na kale, wengine kutwezwa na kuchukizwa kale na kale. Ndipo, wafunzi watakapoangaza kama mwangaza wa mbinguni, nao walioongoza wengi, wapate wongofu, wataangaza kama nyota kale na kale zamani zote. Nawe wewe Danieli, yafunge haya maneno, nacho kitabu kitie muhuri, mpaka siku za mwisho zitakapotimia! Ndipo, wengi watakapokichunguza, utambuzi wao uongezeke. Mimi Danieli nilipotazama nikaona wengine waliosimama hapo, mmoja upande wa huku ukingoni kwa hilo jito, mmoja upande wa huko ukingoni kwa hilo jito. Mmoja akamwuliza yule mume aliyevaa nguo nyeupe ya ukonge aliyesimama juu ya maji ya hilo jito: Itakuwa mpaka lini, mwisho wa maajabu hayo utakapotimia? Nikamsikia yule mume aliyevaa nguo nyeupe ya ukonge, aliyesimama juu ya maji ya hilo jito, akauinua mkono wake wa kuume nao wa kushoto kuielekeza mbinguni, akaapa na kumtaja yule Mwenye uzima wa kale na kale kwamba: Bado kipande cha siku na vipande vya siku na nusu; hapo nguvu za mikono yao walio wa ukoo mtakatifu zitakapokwisha kupondeka, ndipo, hayo yote yatakapotimizwa. Nikayasikia mimi, lakini sikuyatambua, nikamwuliza: Bwana wangu, mwisho wa mambo hayo utakuwaje? Akasema: Jiendee, Danieli! Kwani maneno haya yamefungwa na kutiwa muhuri, mpaka siku za mwisho zitakapotimia. Wengi watatakaswa na kueuliwa kwa kuyeyushwa, lakini wasiomcha Mungu watafanya maovu yao. Kwao hao hatakuwako hata mmoja atakayeyatambua hayo; ndio watakaoyatambua ni wao wenye ujuzi. Tangu hapo, matambiko ya kila siku yatakapoondolewa, mahali pao pawekwe mwangamizaji atapishaye, ni siku 1290. Mwenye shangwe atakuwa angojeaye, afikishe siku 1335! Basi, wewe jiendee, uufikie mwisho! Utatulia, upate kuliinukia fungu lako, siku za mwisho zitakapotimia. Hili ni neno la Bwana lililomjia Hosea, mwana wa Beri, Uzia na Yotamu na Ahazi na Hizikia walipokuwa wafalme wa Wayuda, naye Yoroboamu, mwana wa Yoasi, alipokuwa mfalme wa Waisiraeli. Hapo, Bwana alipoanza kusema na Hosea, Bwana akamwambia Hosea: Nenda, ujichukulie mwamamke mgoni, ujipatie nao watoto wa ugoni! Kwani nchi hii inafuata ugoni kwa kumwacha Bwana. Akaenda, akamchukua Gomeri, binti Dibulemu; naye akapata mimba, akamzalia mwana wa kiume. Bwana akamwambia: Mwite jina lake Izireeli! Kwani kiko bado kitambo kidogo, ndipo, nitakapoulipisha mlango wa Yehu damu za Izireeli na kuukomesha ufalme wa Isiraeli. Siku ile ndipo, nitakapouvunja upindi wa Isiraeli katika bonde la Izireeli. Kisha akapata mimba tena, akazaa mwana wa kike. Bwana akamwambia: Mwite jina lake Hahurumiwi! Kwani sitawahurumia tena walio mlango wa Isiraeli nikiendelea kuwaondolea mabaya yao. Lakini walio mlango wa Yuda nitawahurumia na kuwaokoa kwa nguvu za Bwana Mungu wao, nisiwaokoe kwa nguvu za pindi wala za panga wala za mapigano wala za farasi, wala kwa nguvu za wapanda farasi. Alipokuwa amemzoeza Hahurumiwi, asinyonye maziwa, akapata mimba tena, akazaa mwana wa kiume. Bwana akamwambia: Mwite jina lake Si ukoo wangu! Kwani ninyi ham ukoo wangu, nami sitakuwa tena wenu. Lakini tena hesabu ya wana wa Isiraeli itakuwa kama mchanga wa ufukoni usiopimika wala usiohesabika; itakuwa hapo, hao wanaoambiwa sasa: Ninyi ham ukoo wangu waambiwe: M wanawe Mungu aliye Mwenye uzima. Ndipo, wana wa Yuda na wana wa Isiraeli watakapokusanyika pamoja, wajiwekee kichwa kimoja, wakitoka kwao, waje hapo, kwani siku ile ya Izireeli itakuwa kuu. Hapo waiteni ndugu zenu Ukoo wangu na maumbu zenu Huhurumiwa! Mgombezeni mama yenu! Haya! Mgombezeni! Kwani yeye siye mke wangu, nami si mumewe. Na auondoe ugoni wake, usiwe mbele yake, nao uzinzi wake, usiwe penye maziwa yake, nisije kumvua, akawa mwenye uchi, na kumweka, awe, kama alivyokuwa siku ile, alipozaliwa, nikamgeuza kuwa kama nyika, nikamfanya kuwa kama nchi kavu nikimwua kwa kiu. Nao wanawe sitawahurumia, kwani ndio wana wa ugoni; kwa kuwa mama yao amefanya ugoni, akatenda yenye soni yeye aliyewachukua mimba, maana alisema: Nitawafuata wapenzi wangu wanipao chakula changu na maji yangu, nayo manyoya yangu ya kondoo na pamba zangu, nayo mafuta yangu na vinywaji vyangu. Kwa hiyo utaniona, nikiiziba njia yako kwa miiba, nitajenga hata ukuta, asione pake pa kupitia. Atakapowakimbilia wapenzi wake, asiwafikie, atakapowatafuta, asiwaone; ndipo, atakaposema: Na nije kumrudia mume wangu wa kwanza, kwani hapo naliona mema kuliko sasa. Naye hajui, ya kuwa ni mimi niliyempa zile ngano na zile pombe na yale mafuta, ya kuwa ni mimi niliyemzidishia fedha na dhahabu, walizomtolea Baali. Kwa hiyo na nirudi kuzichukua ngano zangu, siku zitakapotimia, nazo pombe zangu, pangu patakapotimia, nitampokonya nguo zangu za manyoya ya kondoo na za pamba, alizo nazo za kuufunika uchi wake. Sasa nitayafunua yake yenye soni machoni pa wapenzi wake, tena hakuna mtu atakayemponya mkononi mwangu. Nitazikomesha furaha zake zote na sikukuu zake za miandamo ya mwezi nazo za mapumziko na mikutano yake yote. Nitaiharibu mizabibu yake na mikuyu yake, aliyoisema: Hii ndiyo kipaji, wapenzi wangu walichonipa; nitaigeuza kuwa misitu, nyama wa porini waile. Nitampatilizia siku za kuvitambikia vinyago vya Baali, alivyovivukizia uvumba alipojipamba na kuvaa pete zake na ushanga wake akiwafuata wapenzi wake kwa kunisahau mimi; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwa hiyo mtaniona, nikimbembeleza na kumpeleka nyikani, niseme naye kimoyomoyo. Ndiko, nitakakompa mizabibu yake, akitoka huko, nalo Bonde la Akori nitaligeuza kuwa mlango wa kingojeo; ndipo, atakapoitika kama hapo, alipokuwa kijana, alipotoka katika nchi ya Misri kuja huku. Ndivyo asemavyo Bwana: Siku hiyo ndipo, utakaponiita Mume wangu, usiniite tena Bwana wangu. Ndipo, nitakapoyaondoa majina ya vinyago vya Baali kinywani mwako, visitajwe tena kwa majina yao. Siku hiyo nitawafanyia agano nao nyama wa porini n ndege wa angani na wadudu wa nchini, nitayavunja mata na panga na magombano, yatoke katika nchi hiyo, niwakalishe salama. Nitakuposa, uwe wangu kale na kale, nitakuposa, uwe wangu kwa mashauri yaongokayo na kwa huruma zenye upole. Nitakuposa, uwe wangu kwa kweli; ndipo, utakapomjua Bwana. Siku hiyo ndipo, nitakapoitikia; ndivyo, asemavyo Bwana; nitaziitikia mbingu nazo zitaiitikia nchi hii. Nayo nchi hii itaziitikia ngano, nazo pombe na mafuta, nayo hayo yatamwitikia Izireeli (Mungu mpanzi). Nami nitampanda katika nchi hii, awe wangu, nimhurumie Hahurumiwi, tena nitamwambia Si ukoo wangu: Ndiwe Ukoo wangu, naye atasema: Ndiwe Mungu wangu. Bwana akaniambia: Nenda tena kumpenda mwanamke mzinzi anayependwa na mwingine, kama Bwana anavyowapenda wana wa Isiraeli, nao huigeukia miungu mingine kwa kuyapenda maandazi ya zabibu. Nikamnunua, awe wangu, nikatoa fedha kumi na tano na frasila kumi na tano za mawele. Nikamwambia: Siku nyingi utakaa tu kwangu, usizini, wala usiwe wa mume; mimi nami nitakuwa vivyo hivyo kwako. Kwani wana wa Isiraeli watakaa siku nyingi pasipo mfalme wala mkuu, pasipo tambiko wala kinyago, pasipo vazi la mtambikaji wala Patakatifu. Kisha wana wa Isiraeli watarudi, wamtafute Bwana Mungu wao na Dawidi, mfalme wao; siku zitakazokuwa za mwisho watamwendea Bwana na wema wake kwa kutetemeka. lisikieni neno la Bwana, ninyi wana wa Isiraeli! Kwani Bwana yuko na neno la kuwagombeza wakaao katika nchi hii, kwa kuwa hakuna welekevu wala huruma, wala ujuzi wa Mungu katika nchi hii. Huapiza, huongopa, huua, huiba, huvunja unyumba, hukorofisha; ndivyo, damu zinavyoshikamana na damu nyingine. Kwa hiyo nchi hii inasikitika, wakafifia wote wakaao humo, nyama wa porini na ndege wa angani, nao samaki wa baharini wanatoweka. Lakini hawataki, mtu awagombeze, wala mtu awaonye, walio ukoo wako hufanana nao, wanaowagombeza watambikaji. Kwa hiyo utajikwaa mchana, naye mfumbuaji atajikwaa pamoja na wewe usiku, nami nitamwangamiza mama yako. Walio ukoo wangu wanaangamia kwa kukosa ujuzi, kwa kuwa wewe umeukataa ujuzi, nami nakukataa, usinitambikie tena; kwa kuwa umeyasahau Maonyo ya Mungu wako, nami nitawasahau wanao. Hivyo, walivyoendelea kuwa wengi, ndivyo, walivyoendelea kunikosea, kwa sababu hii nitaugeuza utukufu wao kuwa mambo yatiayo soni. Hujilisha makosa yao walio ukoo wangu, namo rohoni mwao hutamani kukora manza kama wao. Kwa hiyo watu na watambikaji watapatwa na mambo yaleyale, nitawapatilizia njia zao, nayo matendo yao nitawarudishia. Watakapokula, hawatashiba; watakapofanya ugoni hawatapata wana, kwa kuwa wameacha kushikana na Bwana. Ugoni na mvinyo na pombe huichukua mioyo yao. Walio ukoo wangu huzipiga mbao zao, nazo fimbofimbo zao huziagulia, kwani roho ya ugoni imewapoteza, wakafanya ugoni papo hapo walipomwacha Mungu wao. Hutambika milimani juu, kwenye vilima huvukiza kuliko na mvule au mgude au mkwaju, kwani kivuli chake ni chema. Kwa hiyo wana wenu wa kike huzini, nao wachumba wenu huvunja unyumba. Sitawapatiliza wana wenu wa kike, ya kuwa huzini, wala wachumba wenu, ya kuwa huvunja unyumba; kwani wenyewe hujitenga, wawe nao wanawake wagoni, hutambika pamoja na wanawali watakatifu wa kimizimu; ndivyo, watu wasiotambua maana wanavyoponzwa. Wewe Isiraeli, ukiwa unafanya ugoni, usimkoseshe Yuda! Msije Gilgali! Wala msipande kwenda Beti-Aweni! Wala msiape na kusema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima! Ikiwa Isiraeli ameshupaa vibaya kama ndama wenye ushupavu, je? Bwana atamchunga kama kondoo penye lisho pana? Efuraimu ni mpenda vinyago, mwache tu! Wakiisha kulewa hufuata ugoni, nao watu wake walio washika ngao hupenda sana mambo yenye soni. Upepo utawakamata kwa ajili ya matambiko yao. Yasikieni haya, ninyi watambikaji! Yasikilizeni, nanyi mlio mlango wa Isiraeli! Nanyi wa mlango wa mfalme, yategeni masikio! Kwani liko shauri linalowataka, kwa maana mmekuwa tanzi la kuwanasa Wamisipa na wavu uliotegwa Tabori juu. Wakachimba mwina mrefu Setimu, lakini mimi nitawachapa wote. Mimi ninamjua Efuraimu, naye Isiraeli hafichiki, nisimwone, kwani hata sasa, wewe Efuraimu, unaufuata ugoni, naye Isiraeli amejipatia uchafu. Matendo yao yanawazuia kurudi kwa Mungu wao, kwani roho ya ugoni imo mioyoni mwao, lakini Bwana hawamjui. Majivuno ya Isiraeli huwaumbua usoni pake; Isiraeli na Efuraimu watajikwaa kwa ajili ya manza, walizozikora, naye Yuda atajikwaa pamoja nao. Huchukua kondoo na ng'ombe kwenda kumtafuta Bwana, lakini hawamwoni, amekwisha kutengana nao. Bwana wamemwacha kwa udanganyifu, wakazaa wana wasio wake. Sasa mwezi utakaoandama utawala pamoja na fungu lao. Pigeni mabaragumu huko Gibea! Pigeni matarumbeta huko Rama! Pigeni yowe Beti-Aweni: Ni nyuma yako, Benyamini! Siku, Efuraimu atakapochapwa, atageuzwa kuwa mapori yaliyo peke yao; niliyoyajulisha mashina ya Isiraeli yatatimia kweli. Wakuu wa Yuda wanafanana nao wanaosogeza mawe ya mipakani; wao hao nitawamwagia machafuko yangu kama maji. Efuraimu anakorofishwa, amepondwa na hukumu, kwani alikuwa amependezwa kufuata maagizo ya watu. Mimi kwake Efuraimu ni kama mende, nako kwao walio mlango wa Yuda kama ugonjwa wa ubovu. Efuraimu alipouona ugonjwa wake, Yuda naye alipouona usaha wa madonda yake, ndipo, Efuraimu alipokwenda Asuri, naye akatuma kwa mfalme Yarevu (Mgombeaji), lakini hataweza kuwaponya, wala hataukausha usaha wenu. Kwani mimi kwake Efuraimu ni kama simba, nako kwao walio mlango wa Yuda kama mwana wa simba, mimi, kweli mimi mwenyewe nitanyafua, kisha nitakwenda zangu; nitakapochukua, hapatakuwapo atakayeopoa. Nitakwenda kurudi mahali pangu, mpaka watakapojutia, wautafute uso wangu; kwa kusongeka kwao watanichungulia usiku kucha. Njoni, tumrudie Bwana! Yeye aliyeturarua ndiye atakayetuponya, yeye aliyetupiga ndiye atakayetufunga vidonda. Ataturudisha uzimani, siku mbili zitakapopita. Siku ya tatu atatuinua; ndipo, tutakapokuwa wazima mbele yake, ndipo, tutakapojua maana, tujihimize kumjua Bwana; hana budi kutokea, kama mapambazuko yasivyokuwa na budi kutokea; atatujia kama mvua, kama mvua ya vuli inyweshayo nchi. Nikufanyizie nini wewe Efuraimu? nikufanyie nini, wewe Yuda? Magawio yenu hufanana na wingu la asubuhi, tena na umande unaokauka mapema. Kwa hiyo nimewapiga kwa wafumbuaji, nikawaua kwa maneno ya kinywa changu, mapatilizo yako hayana budi kutokea kama mwanga; kwani huruma ndizo zitazonipendeza, vipaji vya tambiko sivyo; kumjua Mungu hupita ng'ombe za tambiko, ijapo ziwe za kuteketezwa nzima. Lakini wao kwa kimtu chao huvunja agano; ndivyo, wanavyoniacha kwa udanganyifu. Gileadi ni mji wao wafanyao maovu, nyayo zao hujaa damu. Kama wanyang'anyi wanavyomwotea mtu, ndivyo, chama cha watambikaji kinavyoua katika njia ya kwenda Sikemu; ndiko, walikofanya mabaya, waliyokwisha kuyawaza. Kwao walio mlango wa Isiraeli nimeona mambo yazizimuayo; ndiko, Efuraimu anakofanya ugoni, Isiraeli naye hujichafua. Nawe Yuda, utakayoyavuna, yako tayari; itakuwa hapo, nitakapoyafungua mafungo yao walio ukoo wangu. Ninapotaka kumponya Isiraeli, ndipo, panapotokea wazi manza za Efuraimu na mabaya ya Samaria, kwani hutenda ya uwongo, nao wezi hujipenyeza nyumbani, nako nje huenea wanyang'anyi. Hawasemi mioyoni mwao, ya kama nayakumbuka mabaya yao yote; sasa matendo yao yanawazunguka, yako wazi usoni pangu. Kwa mabaya yao huwafurahisha wafalme wao, nao wakuu wao kwa kuongopa kwao. Wao wote ni wazinzi, hufanana na jiko lililowashwa moto na mchoma mikate, naye akiisha kukanda unga, hupumzika kwa kuchochea moto, hata unga uwe umechachuka. Wakisema: Leo ni sikukuu ya mfalme wetu, ndipo, wakuu wanapojiwasha kwa ukali wa mvinyo; naye mwenyewe hushikana mikono na wafyozaji. Kwa hivyo, wanavyomvizia, humkaribishia mioyo yao, ikiwa yenye moto ulio kama wa jiko la mikate: mchocheaji akiwa amelala usiku kucha, asubuhi huwaka kama moto wenye miali. Hivyo wao wote hupata moto ulio kama wa jiko la mikate, wakawala waamuzi wao, wafalme wao wote wakaangushwa nao, lakini kwao hao hakuonekana aliyenililia mimi. Efuraimu hujichanganya na mataifa mengine, Efuraimu huwa kama andazi lisilogeuzwa. Wageni wamezila nguvu zake, mwenyewe asipovijua; mvi zimemtoka mojamoja, lakini mwenyewe havijui. Majivuno yao Waisiraeli yanawasuta machoni pao, lakini hawarudi kwake Bwana Mungu wao, wala hawamtafuti katika mambo hayo yote. Efuraimu huwa kama hua pumbavu, asiye na akili: mara anamwita Mmisri, mara anakwenda Asuri. Kila mara walipokwenda, niliwatandia wavu wangu, niwanase kama ndege wa angani, kisha nikawapatiliza, kama mkutano wao ulivyoambiwa. Yatawapata, kwa kuwa wamenikimbia! Maangamizo yatawapata, kwa kuwa wamenikosea! Nami nilipotaka kuwakomboa, wao waliniambia ya uwongo tu, hawakunilalamikia kwa mioyo yao, walipolia vitandani kwao. Ni ngano na pombe tu, wanazozikusanyikia, lakini kwangu mimi wameondoka. Tena ni mimi niliyewafunza kuitumia mikono, nikaitia nguvu, lakini huniwazia mabaya tu. Wanaporudi, hawaji kwangu nilioko huku juu, hufanana na upindi uliolegea. Wakuu wao wataangushwa na panga kwa ajili ya ukali wa ndimi zao; kwa hiyo watafyozwa katika nchi ya Misri. Weka baragumu midomoni pako kwamba: Yuko atakayeijia Nyumba ya Bwana kama tai! Wamelivunja Agano langu, wakayakosea Maonyo yangu. Watanililia kwamba: Mungu wetu, sisi Waisiraeli tunakujua! Lakini Isiraeli ameyatupa yaliyo mema, kwa hiyo adui atamkimbiza. Wameweka wafalme, nisiowaagiza mimi, wakaweka wakuu, nisiowajua! Kwa fedha zao na kwa dhahabu zao wakajitengenezea vinyago, kusudi viangamizwe tu. Ndama yako, Samaria, nimeitupa, makali yangu yakapata kuwaka kwa ajili yao. Mpaka lini wataweza kuendelea hivyo pasipo kutakaswa? Ilitokea kwao Waisiraeli, ni fundi aliyeitengeneza, siyo Mungu, kwani itakuwa vumbi hiyo ndama ya Samaria. Kwa kuwa hupanda upepo, watavuna kimbunga, mbegu zao hazioti majani, hazileti unga; kama zingeuleta, wageni wangeula. Waisiraeli wamekwisha kumezwa: wako kwa wamizimu, wanafanana na chombo kisichopendeza. Kwani ndio walioondoka kwenda Asuri, wakawa kama punda wa porini anayejitembelea peke yake. Efuraimu akajinunulia huko wagoni wampendao; lakini ijapo wawanunue kwa wamizimu, nitawapata na kuwakusanya, nao bado kidogo watagaagaa kwa kuumizwa na mizigo, ambayo mfalme na wakuu waliwapagaza. Kwani Efuraimu amejipatia pengi pa kutambikia kwa ajili ya kukosa kwao, napo hapo pa kutambikia pakawa pao pa kukosea. Ijapo nimwandikie mara elfu Maonyo yangu, huwaziwa kwake kuwa mambo mageni tu. Wakitoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima hula nyama, Bwana hapendezwi nao; sasa atazikumbuka manza zao, awapatilizie makosa yao, nao watarudi Misri. Isiraeli alipomsahau Muumbaji wake, alijenga majumba makuu; Yuda naye akajenga miji mingi yenye maboma. Nami nitatia moto mijini mwake, uyale yale majumba yake matukufu. Usifurahi, Isiraeli ukishangilia kama makabila mengine! Kwani umefanya ugoni, ulipomwacha Mungu wako, ukaupenda mshahara wa ugoni po pote, ngano zilipopurwa. Lakini wala purio la ngano wala kamulio la zabibu hayatawachunga, nazo pombe zitawadanganya tu. Hawatakaa katika nchi ya Bwana, Efuraimu atarudi Misri, nako Asuri watakula yenye uchafu. Hawatamtolea Bwana mvinyo za tambiko, wala vipaji vyao vingine vya tambiko havitamfurahisha, kwao wenyewe vitakuwa kama vilaji vya matanga, wote watakaovila watajipatia uchafu, kwani ni vilaji vyao vya kukomesha njaa tu, haviingii Nyumbani mwa Bwana. Mtafanya nini, itakapokuwa siku ya mkutano au sikukuu ya Bwana? Kwani mtaona: waliokwenda zao kwa kukimbia maangamizo Misri itawakusanya, namo Mofu (Memfisi) watawazika, mapambo yao mazuri ya fedha yatatwaliwa na viwawi, mangugi nayo yatakuwa mahemani mwao. Siku za mapatilizo zitafika! Siku za malipizi zitafika! Ndipo, Waisiraeli watakapojua, kama mfumbuaji ni mpumbavu, kama mtu wa kiroho ni mwenye wazimu, kwani manza, ulizozikora, ni nyingi, nao upingani wako ni mwingi. Efuraimu ananivizia, Mungu wangu alipo, tanzi la mtega ndege mfumbuaji huliona katika njia zake zote, ndio upingani uliomo nyumbani mwa mungu wake. Wamejitosa katika matendo mabaya kama siku zile za Gibea; atazikumbuka manza zao, atayapatiliza makosa yao. nilipomvumbua Isiraeli, alikuwa kama zabibu nyikani; kama lilivyo tunda la limbuko la mkuyu unaoanza kuzaa, ndivyo, baba zenu walivyokuwa nilipowaona; lakini walipomfikia Baali-Peori, wakajitenga kwangu, watumikie mambo yenye soni, wakawa matapisho kama hayo mambo, waliyoyapenda. Utukufu wao wa Efuraimu utatoweka kwa kuruka kama ndege, kwa kuwa hapatakuwako atakayezaa wala mwenye mimba wala atakayepata mimba. Ijapo wawakuze wana wao, na niwanyang'anye hao wana wao, asisalie hata mtu mmoja atakayekuwapo. Nao wenyewe wataona mambo, nitakapoondoka kwao. Nilipomwona Efuraimu, alikuwa amepandwa pazuri paelekeapo Tiro, lakini Efuraimu naye hana budi kumtolea muuaji watoto wake. Nikisema: Bwana, wape! utawapa nini? Wape matumbo yasiyozaa na maziwa yaliyokauka! Ubaya wao wote ulitimia Gilgali; ndiko, nilikochukizwa nao; kwa huo ubaya wa matendo yao nitawafukuza Nyumbani mwangu, sitaendelea kuwapenda, wakuu wao wote hukataa kutii. Efuraimu alipopigwa, mizizi yao ikanyauka, hawatazaa tena; ijapo wazae, nitawaua nao wapendwa wao, matumbo yao yaliowazaa. Mungu wangu atawatupa, kwani hawakumsikia; ndipo, watakapokuwa wakitangatanga kwa mataifa. Isiraeli ni mzabibu uchipukao vema, uzaao matunda mema; lakini kama matunda yake yalivyo mengi ndivyo, walivyojitengenezea pengi pa kutambikia, kwa wema wa nchi yako waliulinganya wema wa vinyago. Mioyo yao ni midanganyifu, sasa watalipishwa! Yeye atapavunja pao pa kutambikia, aviangamize vinyago vyao. Kwani sasa husema kweli kwamba: Hatuna mfalme! Bwana hatukumcha, naye mfalme atatufanyizia nini? Husema maneno tu, huapa bure wakifanya maagano; basi, nayo mapatilizo yatakua kama mimea yenye uchungu shambani kwenye matuta. Wakaao Samaria huihangaikia ng'ombe ya Beti-Aweni, kweli watu wa huko wanaiombolezea, nao watambikaji wake wanatetemeka kwa ajili yake, kwa ajili ya utukufu wake, kwa kuwa umeondolewa kwao. Nayo yenyewe itapelekwa Asuri kuwa tunzo la mfalme Yarebu; ndipo, soni zitakapomshika Efuraimu, naye Isiraeli atatwezwa kwa ajili ya shauri lake. Mfalme wa Samaria ataangamizwa, awe kama kibanzi majini juu. Navyo vilima vya Aweni vitaangamizwa, Isiraeli alikomkosea Mungu; miti yenye miiba na mibigili itakulia hapo pao pa kutambikia; ndipo, watakapoiambia milima: Tufunikeni! nayo machuguu: Tuangukieni! Kuanzia zile siku za Gibea umekosa wewe Isiraeli! Huko walisimama, vita vya kuwapiga wapotovu visiwafikie huko Gibea. Nitawapiga, kama itakavyonipendeza; makabila mengine yatawakusanyikia, watakapofungiwa manza zao mbili, walizozikora. Efuraimu anafanana na ndama aliyefundishwa, apendaye kupura; nami nitautumia uzuri wa shingo yake na kumfundisha kuvuta gari; hata Yuda atalima mahali pa ng'ombe, naye Yakobo atajipondea mwenyewe madongo. Kwa hiyo jipandieni yatakayoleta wongofu, mpate kuvuna yenye utu! jilimieni shamba jipya, siku zingaliko bado za kumtafuta Bwana, mpaka aje na kuwafundisha yanyokayo! Lakini ninyi hulimia mabaya, mkavuna mapotovu, mkala mazao ya uwongo. Kwa kuwa unajishikiza kwa njia yako na kwa wingi wa watu walio na nguvu za kupiga vita, kwa hiyo makelele ya vita yatatokea kwa watu wako, nayo miji yako yote yenye maboma itaangamizwa, kama Salmani alivyouangamiza Beti-Arbeli siku, walipopigana, ni hapo wamama waliposetwa na kuuawa pamoja na watoto. Mambo kama hayo ndiyo, Beteli utakayowapatia ninyi, kwa ajili ya ubaya wenu ulio mwingi; siku moja kutakapopambazuka, mfalme wa Isiraeli atakuwa ameangamia kabisa. Isiraeli alipokuwa kijana, nilimpenda; huko Misri ndiko, nilikomwitia mwanangu. Lakini walipowaita halafu, ndipo, walipokwenda zao na kutoka kwao hao, wakayatambikia Mabaali na kuvukizia vinyago. Nami mwenyewe nalimfundisha Efuraimu kwenda kwa miguu kama mtoto, nikawashika mikono, lakini hawakutambua, ya kuwa ninawaponya. Naliwavuta kwa kamba zimfaazo mtu na kwa vigwe vya upendo, nikawa nikiwatua mizigo mabegani pao, nikawainamia, nipate kuwalisha chakula. Hawatarudi katika nchi ya Misri, ila Mwasuri ndiye atakayekuwa mfalme wao, kwani wamekataa kurudi kwangu. Nazo panga zitazunguka mijini mwao, ziyamalize makomeo yao kwa kuyala kwa ajili ya mashauri yao. Walio ukoo wangu hujipingia kuniacha; wakiitwa kurudi kwake Alioko huko juu, kwao wote hakuna atakayemtukuza. Nitawezaje kukutoa Efuraimu au kukuacha, Isiraeli? Nitawezaje kukutoa, uwe kama Adima (Sodomu), au kukugeuza, uwe kama Seboimu (Gomora)? Moyo wangu ungefudikizwa kifuani mwangu, ungechafuka sana kwa kukuonea uchungu. Sitayafanya, ukali wangu wenye moto uyatakayo, sitamwangamiza tena Efuraimu, kwani mimi ni Mungu, si mtu; namo katikati yenu mimi ni mtakatifu, nisije kuingia kwenu kwa machafuko. Watakuja kumtafuta Bwana, atakaponguruma kama simba; kweli atakaponguruma, ndipo, watakapokuja kwa kutetemeka wao watoto watokao upande wa baharini. Watamkimbilia kama ndege kwa kutetemeka wakitoka Misri, au kama hua wakiitoka nchi ya Asuri; ndipo, nitakapowakalisha nyumbani mwao; ndivyo, asemavyo Bwana. Efuraimu amenizingia uwongo, walio mlango wa Isiraeli wamenizingia udanganyifu; Yuda naye hata sasa hujiendea na kumwacha Mungu aliye mtakatifu na mwelekevu. Efuraimu hujilisha upepo, huukimbilia upepo utokao maawioni kwa jua, siku kwa siku huongeza uwongo na uangamizo: hufanya maagano na Asuri, tena mafuta hupelekwa Misri. Lakini Bwana yuko na shauri na Yuda, ampatilizie Yakobo njia zake na kumlipisha matendo yake. Tumboni mwa mama alimshika kaka yake kisigino, napo, alipokuwa mtu mzima, alishindana na Mungu. Akashindana na malaika, akamshinda kwa kulia na kumlalamikia; Beteli ndiko, alikomwona, ndiko, alikosema na sisi yeye Bwana Mungu Mwenye vikosi; Bwana ni Jina lake la kumtukuza. Nawe sharti urudi kwa Mungu wako, ushikamane na upole, ufanye yapasayo, umngojee Mungu wako pasipo kukoma. Kwa kushika mizani ya kudanganyia mikononi mwake Mkanaani hupenda kukorofisha. Efuraimu husema: Kumbe ni tajiri! Nimejipatia mali! Tena kwa hivyo vyote, nilivyovisumbukia, hawataniona, ya kuwa nimefanya kiovu cha kumkosea mtu. Lakini mimi Bwana ni Mungu wako tangu hapo, nilipokutoa katika nchi ya Misri, mimi nitakukalisha tena katika mahema kama penye sikukuu za mkutano. Mimi nilisema na wafumbuaji, nikawatokea mara nyingi, nikawaonya kwa vinywa vya wafumbuaji na kusema mifano. Kwa kuwa huko Gileadi walifanya yasiyofaa, basi, nao watageuzwa kuwa si kitu; kwa kuwa huko Gilgali walitoa ng'ombe za tambiko, napo pao pa kutambikia patakuwa kama chungu za mawe penye matuta. Yakobo alikimbilia mashamba ya Aramu, Isiraeli akatumikia kupata mwanamke, hakuwa na budi kuchunga kondoo na mbuzi, ampate mkewe. Lakini kwa mkono wa mfumbuaji Bwana alimtoa Isiraeli huko Misri, kisha wakachungwa na mfumbuaji. Efuraimu amemsikitisha masikitiko yenye uchungu; kwa hiyo zile damu, alizozimwaga, atamtupia, zimkalie, nayo matusi yake ndiyo, Bwana wake atakayomlipisha. Efuraimu aliposema, watu walitetemeka; kwani alikuwa mkuu kwao Waisiraeli. kisha akakora manza kwa kumtumikia Baali, basi akafa. Na sasa wanaendelea kukosa wakijifanyizia vinyago kwa fedha zao, vingine wanavichonga, kama wanavyojua; vyote pia ni kazi za mafundi. Kwa ajili yao wenyewe husema: Watoao watu kuwa ng'ombe zao za tambiko sharti wanonee ndama! Kwa sababu hiyo watakuwa kama wingu la asubuhi na kama umande ukaukao upesi, au kama makapi yanayopeperushwa penye kupuria au kama moshi utokao katika bomba. Lakini mimi Bwana ni Mungu wako tangu hapo, nilipokutoa katika nchi ya Misri; nawe usijue mungu mwingine ila mimi, hakuna mwokozi, nisipokuwa mimi. Mimi nilikujua ulipokuwa nyikani katika nchi kavu yenye kiu. Lakini walipoona malisho mema wakashiba; napo waliposhiba, mioyo yao ikajikuza, kwa hiyo wamenisahau. Ndipo, nilipowageukia kuwa kama simba, nikawavizia kama chui njiani, niwarukie kama nyegere aliyenyang'anywa watoto, niwapasue vifua vifunikavyo mioyo yao, niwale hapo hapo kama simba jike, kisha nyama wa porini wawanyafuenyafue, Haya ndiyo yanayokuangamiza, Isiraeli, ya kuwa unanikataa mimi niliye msaada wako Mfalme wako yuko wapi, akuokoe katika miji yako yote? Wako wapi waamuzi wako, uliowaambia: Nipeni mfalme na wakuu! Mimi nilikupa mfalme kwa kukasirika kwangu, tena nikamwondoa kwa makali yangu yenye moto. Manza zake Efuraimu zimefungwa pamoja, makosa yake yakawekwa fichoni. Uchungu wa mzazi utamjia, lakini yeye ni mwana asiyejua kitu; saa yake itakapofika, haji kusimama hapo, wana wanapotokea tumboni mwa mama. Nitawakomboa katika nguvu za kuzimuni na kuwaokoa kufani. Wewe Kifo, magonjwa yako yauayo yako wapi? Wewe Kuzimu, uchungu wako uko wapi? Ndipo, yawezayo kujutisha yatakapokuwa yamefichwa, macho yangu yasiyaone. Lakini ijapo awe mwenye kuzaa miongoni mwa ndugu zake, pumzi ya Bwana itamjia kuwa upepo utokao maawioni kwa jua upande wa nyikani, kisima chake kikauke, nacho kijito chake kipwe. Yule ndiye atakayeviteka vilimbiko vyote vya vyombo vyote pia vipendezavyo. Samaria atalipishwa manza, alizozikora kwa kumpingia Mungu wake: kwa hiyo wataangushwa kwa panga, watoto wao wachanga watapondwa, nao wanawake wenye mimba watatumbuliwa. Rudi, Isiraeli, kwa Bwana Mungu wako! Kwani umejikwaa kwa maovu, uliyoyafanya. Yashikeni maneno haya kwenda nayo, mkirudi kwake Bwana, ya kumwambia: Ziondoe manza zote pia, tulizozikora, ututolee wema! Ndipo, tutakapotoa shukrani za midomo yetu, ziwe ng'ombe za tambiko. Mwasuri hawezi kutuokoa, nasi hatujui kupanda farasi; hatutaziita tena kazi za mikono yetu kwamba: Ni mungu wetu! Kwani kwako ndiko, wafiwao na wazazi wanakojipatia huruma. Watakaporudi hivyo, nitawaponya, nitawapenda kwa moyo, kwani ndipo, makali yangu yatakapokuwa yamewaondokea. Ndipo, nitakapokuwa kwake Isiraeli kama umande, apate kuchanua kama maua ya shambani, ashushe mizizi yake kama miti ya Libanoni. Matawi yake yatakuwa marefu, uzuri wake uwe kama wa mchekele, nao utanuka vizuri kama mti wa Libanoni. Watakaokaa kivulini kwake watarudia kupanda ngano, watachanua kama mizabibu, sifa yao itakuwa kama sifa ya mvinyo za Libanoni. Ndipo, Efuraimu atakaposema: Vinyago vinanifaliaje tena? Nami nitamjibu na kumtazama kwa kupendezwa: Mimi ni kama mvinje mbichi, kwangu mimi kutaonekana yaliyo mazao yako. Yuko nani aliye mwerevu wa kweli, ayatambue hayo? Yuko nani aliye mtambuzi, ayajue maana yao hayo? Kwani njia za Bwana hunyoka, nao waongofu huzishika, lakini wapotovu hukwazwa nazo. Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Yoeli, mwana wa Petueli: Yasikieni haya, ninyi wazee! Yasikilizeni, ninyi nyote mkaao katika nchi hii! Je? Kama hayo yamefanyika katika siku zenu au katika siku za baba zenu? Yasimulieni haya wana wenu! Nao wana wenu wayasimulie wana wao! Nao wana wao wayasimulie uzao mwingine ujao! Panzi waliyoyasaza yameliwa na nzige, nzige waliyoyasaza yameliwa na funutu, funutu waliyoyasaza yameliwa na bumundu. Levukeni, ninyi walevi, kalieni! Pigeni kelele, nyote mnywao mvinyo! Ni kwa ajili ya mvinyo mbichi, kwa kuwa zimekwisha kuondolewa vinywani mwenu! Kwani liko kabila, limepanda kuiingia nchi yangu, ni lenye nguvu, tena halihesabiki, meno yao kama meno ya simba, magego yao kama ya simba jike. Wameigeuza mizabibu yangu, iwe kama jangwa, nayo mikuyu yangu, iwe mashina matupu, wameyabandua maganda yao, wakayatupa chini, matawi yao yakawa meupe kabisa. Ombolezeni kama mwanamwali aliyejivika gunia kwa ajili ya bwana wa ujana wake! Vilaji na vinywaji vya tambiko vimekomeshwa, visifike Nyumbani mwa Bwana; kwa hiyo watambikaji wanasikitika, ndio wanaomtumikia Bwana. Mashamba yameangamizwa, nchi imesikitika, kwani ngano zimeangamia, mvinyo mpya zimekupwa, mafuta nayo yamefifizwa. Wakulima wametwezwa, watunza mizabibu wanalia, kwa ajili ya ngano na ya mawele, kwani ngano zimeangamia, mvinyo mpya zimekupwa, mafuta nayo yamefifizwa. Wakulima wametwezwa, watunza mizabibu wanalia, kwa ajili ya ngano na ya mawele, kwani mavuno ya mashamba yamepotea. Mizabibu imekauka, mikuyu imefifia, mikomamanga na mitende na michungwa, miti yote pia ya shambani imekauka, kweli nazo furaha zimekaukiana, zimewapotelea watu. Vaeni nguo za matanga! Ombolezeni, ninyi watambikaji! Pigeni kelele, mnaotumikia mezani pa kutambikia! Njoni, mlale usiku kucha na kuvaa magunia, mnaomtumikia Mungu wangu! Kwani Nyumba ya Mungu wenu imenyimwa vilaji na vinywaji vya tambiko! Eueni mfungo! Utangazeni mkutano! Wakusanyeni wazee nao wote wanaokaa katika nchi hii, waje Nyumbani mwa Bwana Mungu wenu, mmlalamikie Bwana! Semeni: Imetupata ile siku! Kweli siku ya Bwana iko karibu! Inakuja kama mwangamizo utokao kwake Mwenyezi! Je? Chakula hakikuondolewa machoni petu? Nyumbani mwa Mungu wetu hamkuondoka furaha na shangwe? Mbegu zimenyauka chini ya madongo yao, vilimbiko vimetoweka, vyanja vimebomolewa, kwani ngano zimekauka! Sikilizeni! Nyama nao wanapiga kite! Makundi ya ng'ombe yametatizwa, kwani hakuna malisho yao, nayo makundi ya kondoo yanakosa. Wewe Bwana, ninakulilia, kwani moto umezila mbuga za nyikani, moto wenye miali umeichoma miti yote ya porini. Nao nyama wa porini wanakutwetea kwani vijito vya maji vimekauka, nao moto umezila mbuga za nyikani. Pigeni baragumu Sioni! Pigeni kelele milimani kwenye utakatifu wangu! Wote wakaao katika nchi hii watetemeke, kwa kuwa siku ya Bwana inakuja, iko karibu! Ni siku yenye giza lililozidi kabisa, ni siku yenye mawingu yaliyo meusi; kama wekundu wa kupambazuka unavyotandama milimani juu, ndivyo, lile kabila linavyotokeza wengi walio wenye nguvu; walio kama hao hawakuwako toka kale, wala hawatakuwako tena nyuma yao hata miaka ya vizazi na vizazi. Mbele yao moto unakula, nyuma yao miali ya moto inawaka; mbele yao nchi ni kama bustani ya Edeni, nyuma yao ni jangwa tupu, pasipatikane pa kuponea. Ukiwatazama, wanafanana kuwa kama farasi, wanapiga mbio kama wapanda farasi. Uvumi wao ni kama wa magari yarukayo milimani juu au kama uvumi wa moto ulao majani makavu; ni kama wa watu wenye nguvu waliojipanga kupigana. Mbele yao watu wanajipinda, nyuso zao zikiwapoa. Wanapiga mbio kama wenye nguvu wa vitani, wanakwea ukutani kama mafundi wa mapigano, wanakwenda kila mmoja katika njia yake, hawayapotoi kamwe mapito yao, wala hawasukumani wenyewe mtu na ndugu yake, kila mmoja huendelea katika mkondo wake; ingawa wengine wao waanguke kwa kupigwa, hawazuiliki. Wanaurukia mji wakizikwea kuta za bomani mbiombio, wanapanda kuingia nyumbani na kujipenyeza madirishani kama mwizi. Mbele yao nchi inatetemeka, nazo mbingu zinatikisika, jua na mwezi unaguiwa na giza, nazo nyota zinakoma kuangaza. Bwana anapiga ngurumo yake, ivitangulie vikosi vyake, kwa kuwa kambi lake ni kubwa sana, nao walitimizao neno lake ni wenye nguvu; kwani siku ya Bwana ni kuu, inaogopesha sana, yuko nani atakayeivumilia? Ndivyo, asemavyo Bwana: Sasa hivi rudini kwangu kwa mioyo yenu yote mkifunga kwa kulia na kuomboleza! Irarueni mioyo yenu, msiyararue mavazi yenu! Kisha rudini kwa Bwana Mungu wenu! Kwani Yeye ni mwenye utu na huruma, tena mwenye uvumilivu na upole mwingi; hugeuza moyo, asifanye mabaya. Labda atageuza moyo tena, atuachilie mbaraka atakapoondoka, akiwapatia vilaji na vinywaji vya kumtambikia Bwana mungu wenu! Pigeni baragumu Sioni! Eueni mfungo! Utangazeni mkutano! Wakusanyeni watu wa kwenu! Ueueni huo mkutano! Waiteni wazee! Wakusanyeni nao wachanga, nao wanyonyao maziwa! Mchumba mume atoke chumbani mwake! Naye mchumba mke atoke mwake, alimo! Watambikaji wanaomtumikia Bwana na walie katikati ya ukumbi na meza ya kutambikia, waseme: Bwana, wahurumie walio ukoo wako! Usiwatoe walio fungu lako, watukanwe, wamizimu wakiwatawala! Mbona wataka, waseme kwa makabila mengine: Mungu wao yuko wapi? Ndipo, Bwana alipoionea nchi yake wivu, akawahurumia walio ukoo wake. Bwana akajibu na kuwaambia walio ukoo wake: Mtaniona, nikiwapatia ngano na pombe mbichi na mafuta, myashibe! Sitawatoa tena, mtukanwe na wamizimu. Nao wale waliotoka kaskazini nitawaondoa kwenu, niwapeleke mbali, niwakumbe, waende katika nchi kavu iliyo peke yake; watangulizi wao nitawatupa katika bahari iliyoko upande wa maawioni kwa jua, wafuasi wao wa nyuma nitawatupa katika bahari iliyoko upande wa machweoni kwa jua, mnuko mbaya wa kuoza kwao utapanda juu, kwa sababu watakuwa wamefanya makuu zaidi. Usiogope, wewe nchi! Ila shangilia kwa furaha! Kwani Bwana atafanya jambo kuu. Msiogope, ninyi nyama wa porini! Kwani mbuga za nyikani zitachipuka, kwani miti itazaa matunda yao, nayo mikuyu na mizabibu itatoa mazao ya nguvu. Wana wa Sioni, shangilieni! Mfurahieni Bwana Mungu wenu! Kwani anawapa mvua ya masika hapo ipasapo, anawanyeshea kwanza mvua za masika nazo za vuli. Ndipo, penye kupuria patakapojaa ngano, nayo makamulio yatafurikiwa na mvinyo mbichi na mafuta. Nitawarudishia miaka iliyoliwa nao nzige na funutu na bumundu na panzi, ni vile vikosi vyangu vingi vyenye nguvu, nilivyovituma kwenu. Mtakula kabisa na kushiba, mlisifu Jina la Bwana Mungu wenu, kwa kuwa alifanya kwenu mataajabu! Kweli walio ukoo wangu hawatapatwa na soni kale na kale. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi niko katikati ya Waisiraeli, ya kuwa mimi Bwana ni Mungu wenu, siye mwingine. Kweli walio ukoo wangu hawatapatwa na soni kale na kale. Hayo yatakapokwisha, ndipo, itakapokuwa, niwamiminie Roho yangu wote walio wenye miili ya kimtu. Nao wana wenu wa kiume na wa kike watasema na kufumbua; nao wazee wenu wataoteshwa ndoto, nao vijana wenu wataona maono. Nao walio watumwa wangu waume na wake nitawamiminia Roho yangu siku zilezile. Nami nitafanya vioja mbinguni na nchini, vyenye damu na moto na moshimoshi. Jua litageuka, liwe giza, nao mwezi utageuka, uwe damu mbele ya kutimia kwake ile siku kubwa ya Bwana, inayoogopesha. Tena itakuwa, kila atakayelitambikia Jina la Bwana ataokoka. Kwani mlimani pa Sioni namo Yerusalemu watakuwamo waliopona, kama Bwana alivyosema; namo miongoni mwao waliookolewa watakuwamo, Bwana aliowaita. Siku zile za huo wakati zitakapotimia, mtaniona nikiyafungua mafungo ya Yuda na ya Yerusalemu. Ndipo, nitakapowakusanya wamizimu wote, niwapeleke katika bonde la Yosafati; ndiko, nitakakowakatia shauri kwa ajili ya ukoo wangu wa Isiraeli ulio fungu langu, kwa kuwa wamewatawanya kwenye wamizimu, wakajigawanyia nchi yangu. Wao walio ukoo wangu wamewapigia kura, wakitoa mtoto wa kiume, wajipatie mwanamke mgoni, tena wamenunua mvinyo kwa mtoto wa kike, wakazinywa. Ninyi wa Tiro na wa Sidoni mwanitakiaje? Nanyi nyote mkaao upande wa Wafilisti? Je? Ninyi mwataka kunilipisha niliyofanyiziwa? Au mnacho, mtakacho kunifanyizia? Sasa hivi kwa upesi nitawarudishia matendo yenu, yaje kuwaangukia vichwani penu. Kwani mmezichukua fedha zangu na dhahabu zangu, nayo mapambo mazuri yaliyonipendeza mmeyapeleka katika majumba ya miungu yenu. Nao wana wa Yuda na wa Yerusalemu mmewauzia wana wa Wagriki, mpate kuwapeleka mbali, wasirudi mipakani kwao. Lakini mtaniona, nikiwainua mahali hapo, mlipowauzia, nitakapowarudishia matendo yenu, yaje kuwaangukia vichwani penu. Kisha nitawauza wana wenu wa kiume na wa kike na kuwatia mikononi mwao wana wa Yuda, nao watawauzia Wasaba, kwa kuwa ni taifa likaalo mbali; kwani Bwana ndiye aliyevisema. Yatangazeni haya kwa mataifa! Kisha eueni vita! Wainueni wenye nguvu! Wote walio mafundi wa vita na waje na kujipanga! Yafueni majembe yenu, yawe panga, navyo visu vyenu, viwe mikuki! Naye aliye mnyonge sharti aseme: Mimi ni mwenye nguvu! Pigeni mbio, mje mkusanyike, ninyi mataifa yote mkaao na kuwazunguka! Nawe Bwana, wapeleke wanguvu wako, wawatelemkie kuko huko! Mataifa na waimbe, waje huko bondeni kwa Yosafati! Kwani ndiko, nitakakokaa, niwahukumu wao wa mataifa yote wakaao na kuwazunguka. Haya! Leteni miundu! Kwani mavuno yameiva. Njoni, mkanyage! Kwani kamulio limejaa, mapipa nayo yanamwagikia, kwani mabaya yao ni mengi. Yako makundi ya watu mengi na mengi huko bondeni kunakokatwa mashauri, kwani siku ya Bwana iko karibu huko bondeni kunakokatwa mashauri. Jua na mwezi umeguiwa na giza, nazo nyota zimekoma kuangaza. Ndipo, Bwana atakaponguruma mle Sioni, ataivumisha sauti yake mle Yerusalemu, mbingu na nchi zitetemeke. Lakini Bwana atakuwa kimbilio lao walio ukoo wake na ngome yao walio wana wa Isiraeli. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi Bwana ni Mungu wenu akaaye Sioni penye mlima wangu mtakatifu. Nao Yerusalemu utakuwa mji mtakatifu, msimopita wageni tena. Siku ile itakuwa, milima idondoe mvinyo mbichi, navyo vilima vitachuruzika maziwa, navyo vijito vyote vya Yuda vitaleta maji mengi. Kisha Nyumbani mwa Bwana mtatokea chemchemi, italinywesha Bonde la Migunda. Misri itakuwa mapori tu, nayo Edomu itakuwa nyika yenye mapori matupu, kwa kuwa wamewakorofisha wana wa Yuda, wakamwaga katika nchi yao damu zao wasiokosa. Lakini Yuda itakaa watu kale na kale, namo Yerusalemu watakaa vizazi kwa vizazi. Ndivyo, nitakavyozilipiza damu zao, ambazo sikuzilipiza bado. Naye Bwana atakuwa anakaa Sioni! Maneno ya Amosi aliyekuwa mchunga ng'ombe na kondoo kwao Tekoa; ni mambo yatakayowapata Waisiraeli, naye aliyaona katika siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na za Yoroboamu, mwana wa Yoasi, mfalme wa Isiraeli; ilikuwa miaka miwili kabla ya ule mtetemeko wa nchi Alisema: Bwana atanguruma mle Sioni, ataivumisha sauti yake mle Yerusalemu; ndipo, mbuga za wachungaji zitakaposikitika, nao mlima wa Karmeli utakauka juu yake. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa ajili ya mapotovu ya Damasko matatu au manne sitayarudisha, yasiwapate, kwa kuwa waliupura Gileadi kwa magari ya chuma ya kupuria. Nitatupa moto nyumbani mwa Hazaeli, uyale majumba ya Benihadadi, nitalivunja komeo la Damasko, nitawang'oa wakaao katika Bonde la Maovu, nitamng'oa naye mshika bakora ya kifalme mle Beti-Edeni; nao watu wa Ushami watatekwa na kuhamishwa kwenda Kiri. Bwana ameyasema. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa ajili ya mapotovu ya Gaza matatu au manne sitayarudisha, yasiwapate, kwa kuwa waliwateka wote pia na kuwahamisha, wawapeleke utumwani kwa Waedomu. Nitatupa moto bomani mwa Gaza, uyale majumba yao, nitawang'oa wakaao mle Asdodi, naye mshika bakora ya kifalme mle Askaloni; kisha nitaugeuza mkono wangu, uujie Ekroni, ndipo, Wafilisti waliosalia watakapoangamia. Bwana Mungu ameyasema. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa ajili ya mapotovu ya Tiro matatu au manne sitayarudisha, yasiwapate, kwa kuwa wote pia, waliowateka, waliwahamisha na kuwapeleka kwa Waedomu, hawakulikumbuka agano la Kindugu. Nitatupa moto bomani mwa Tiro, uyale majumba yao. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa ajili ya mapotovu ya Edomu matatu au manne sitayarudisha, yasiwapate, kwa kuwa waliwakimbiza ndugu zao kwa panga, wakajizuia, wasiwahurumie, kwa kuwa waliendelea siku zote kuwanyafua kwa ukali, hawakomi kuwachafukia kale na kale. Nitatupa moto mle Temani, uyale majumba ya Bosira. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa ajili ya mapotovu ya wana wa Amoni matatu au manne sitayarudisha, yasiwapate kwa kuwa waliwatumbua wenye mimba wa Gileadi, wapate kuipanua mipaka yao. Lakini nitawasha moto bomani mwa Raba, uyale majumba yao, wapige makelele, kwa kuwa ni siku ya vita, pawe uvumi, kwa kuwa ni siku ya chamchela. Naye mfalme wao atakwenda kuhamishwa, kwa kuwa atatekwa yeye na wakuu wake. Bwana ameyasema. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa ajili ya mapotovu ya Moabu matatu au manne sitayarudisha, yasiwapate, kwa kuwa mifupa ya mfalme wa Edomu waliichoma moto, hata ikawa chokaa. Nitatupa moto kwao Moabu, uyale majumba ya Kerioti, nao Wamoabu watakufa katika mvurugo, makelele ya vita na milio ya mabaragumu ikisikilika. Naye mwamuzi nitamng'oa katikati yao, nao wakuu wao wote nitawaua pamoja nao. Bwana ameyasema. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa ajili ya mapotovu ya Yuda matatu au manne sitayarudisha, yasiwapate, kwa kuwa wameyakataa Maonyo ya Bwana, wakaacha kuyashika maongozi yake, ikawapoteza miungu yao ya uwongo baba zao waliyoifuata. Nitatupa moto kwao Yuda, uyale majumba ya Yerusalemu. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa ajili ya mapotovu ya Isiraeli matatu au manne sitayarudisha, yasiwapate, kwa kuwa wamewauza waongofu kwa fedha, nao maskini kwa viatu viwili. Wanatunukia na kutwetatweta, mavumbi ya nchi yawe vichwani juu yao wakiwa, nazo njia za wanyonge huzipotoa. Mtu na baba yake pamoja humwendea mwanamke mgoni, Jina langu takatifu walipatie uchafu. Hutumia nguo, walizopewa za kuwekea wengine, hujitandikia zizo hizo pote, wanapotambikia; nyumbani mwa miungu yao hunywa mvinyo zao, walizotozwa kuwa malipo ya makosa. Nami ndimi niliyewaangamiza Waamori mbele yao, ndio waliokuwa warefu kama miangati mirefu na wanguvu kama mivule, nikayaangamiza mazao yao ya juu nayo mizizi yao ya chini. Nami ndimi niliyewatoa katika nchi ya Misri na kuwaleta huku, nikawaongoza miaka arobaini nyikani, nikawapa nchi ya Waamori, iwe nchi yenu. Namo miongoni mwa wana wenu nikainua wengine, wawe wafumbuaji, nao wengine nikawachagua katika vijana wenu, wajieue kuwa wangu. Au sivyo vilivyokuwa, ninyi wana wa Isiraeli? ndivyo, asemavyo Bwana. Nao waliojieua mliwanywesha mvinyo, nao wafumbuaji mkawaagiza kwamba: Msifumbue! Mtaniona, nikiwalemea, kama gari linavyolemewa likijaa miganda. Ndipo, mwenye miguu izoeayo mbio atakaposhindwa na kukimbia, naye mwenye nguvu hataweza kutumia hizo nguvu zake kuu, wala fundi wa vita hataiponya roho yake, wala mshika upindi hatasimama, wala mwenye miguu miepesi hatapona, wala mpanda farasi hataiponya roho yake. Naye aushupazaye moyo wake kwa mafundi wa vita siku hiyo atakimbia akiwa uchi; ndivyo, asemavyo Bwana. Lisikieni neno hili, Bwana alilolisema kwa ajili yenu, ninyi wana wa Isiraeli, kwa ajili ya huu ukoo wote, nilioutoa katika nchi ya Misri na kuuleta huku: Amesema: Niliwajua ninyi tu katika koo zote zilizoko nchini, kwa hiyo nitawapatilizia ninyi manza zote, mlizozikora. Je? Wako wawili wanaosafiri pamoja, isipokuwa wamepatana? Je? Simba ananguruma mwituni, asipokuwa amepata windo? Je? Mwana wa simba analia pangoni mwake, asipokuwa amekamata? Au ndege anawezaje kuanguka tanzini chini, isipokuwa mtu amelitega? Au tanzi linafyatuka na kuruka juu, lisipokuwa limekamata? Au baragumu la vita likipigwa mjini, watu waliomo mjini hawashikwi na woga? Au yako mabaya mjini, Bwana asiyoyafanya? Kweli Bwana Mungu hafanyi neno, asipokuwa amewafunulia njama yake watumishi wake wafumbuaji. Simba akinguruma, yuko nani asiyeogopa? Bwana Mungu akisema neno, yuko nani asiyetaka kulifumbua? Yatangazeni majumbani mwa Adodi! Namo majumbani mwa nchi ya Misri! Semeni: Kusanyikeni milimani kwa Samaria! Itazameni mivurugo, jinsi inavyozidi katikati yao! Yatazameni nayo makorofi yaliyoko huko kwao! Ndivyo, asemavyo Bwana: Hawakujua kufanya yaliyo sawa wao waliolimbika majumbani mwao makorofi na mapokonyo. Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Yuko atakayeisonga nchi hii po pote na kuvibwaga chini vilivyokuwa nguvu zako, majumba yako yapate kutekwa. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kama mchungaji anavyoopoa kinywani mwa simba mifupa miwili ya mguu au kipande cha sikio, ndivyo, watakavyojiponya wana wa Isiraeli wakaao sasa Samaria pembeni kitandani juu ya mito ya hariri ya malalo. Yasikieni, myashuhudie nyumbani mwa Yakobo! ndivyo, asemavyo Bwana Mungu aliye Mungu Mwenye vikosi. Kwani siku hiyo, nitakayowapatilizia Waisiraeli mapotovu yao, ndipo, nitakapowapatilizia napo pa kutambikia Beteli, pembe za hiyo meza ya kutambikia zivunjwe, zianguke chini. Ndipo, nitakapozibomoa nyumba za kupupwe pamoja nazo za kiangazi, navyo vyumba vilivyopambwa na pembe za tembo vitaangamia, hizo nyumba nyingi zitakapotoweka; ndivyo, asemavyo Bwana. Lisikieni neno hili, ninyi ng'ombe wa Basani! Ninyi mlioko milimani kwa Samaria mkiwakorofisha wanyonge na kuwaponda maskini! Ninyi mnaowaambia bwana zao: Haya! Leteni, tunywe! Bwana Mungu ameapa na kuutaja utukufu wake kwamba: Mtaona, siku zikiwajia ninyi, mtakapovutwa juu kwa kulabu, hata masazo yenu yatavutwa juu kwa ndoana za kuvulia samaki. Mtatoka penye nyufa za ukuta, kila mwanamke mmoja ashike njia yake ya kwenda moja kwa moja, mje kujitupa huko Harmoni; ndivyo, asemavyo Bwana. Haya! Nendeni Beteli, mjikoseshe! Nendeni Gilgali, mzidishe kujikosesha! Katoeni asubuhi vipaji vyenu vya tambiko! Hata kila siku ya tatu yatoeni mafungu yenu ya kumi! Chomeni mikate yenye chachu, iwe shukrani! Tangazeni, visikilike, watu watoe vipaji viwapendezavyo! Kwani ndivyo, mnavyovipenda, ninyi wana wa Isiraeli; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Nami niliwapa meno yakosayo kazi mijini mwenu mote nao ukosefu wa mkate pote, mnapokaa, lakini hamkurudi kwangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Tena mimi niliwanyima mvua, miezi mitatu tu ilipokuwa imesalia mpaka mavunoni, mji mmoja nikaunyeshea mvua, tena mwingine sikuunyeshea mvua, shamba moja likanyeshewa na mvua, jingine lisilopata mvua likakauka. Miji miwili mitatu ikatangatanga kuendea mji mmoja tu, ndimo wapate kunywa maji, ijapo wasishibe, lakini hamkurudi kwangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Nikawapiga ninyi, nikayaunguza mashamba na kuyakausha kabisa, tena mara nyingi nzige waliyala kwenu mashamba na mizabibu na mikuyu na michekele yenu, lakini hamkurudi kwangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Nilituma kwenu magonjwa mabaya, kama nilivyovifanya huko Misri, nikawaua vijana wenu kwa panga, nao farasi wenu wakatekwa. Nikaupandisha mnuko mbaya wa kambi zenu, uingie puani mwenu, lakini hamkurudi kwangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Niliwafudikiza wa kwenu, kama Mungu alivyofudikiza Sodomu na Gomora, mkawa kama kijinga kilichopona kwa kuokolewa, kisiteketee chote motoni, lakini hamkurudi kwangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwa hiyo yako, nitakayokufanyizia Isiraeli; jiweke tayari kukutana na Mungu wako, Isiraeli, kwa ajili yao nitakayokufanyzia! Kwani utamwona atengenezaye milima, aumbaye upepo, amwambiaye mtu ayawazayo moyoni mwake, ni yeye ayageuzaye mapema kuwa giza akipita na kukanyaga juu ya vilima vya nchi; Bwana Mungu Mwenye vikosi ni Jina lake. Lisikieni neno hili, ninalowatolea mimi! Ni ombolezo la kuwaombolezea ninyi mlio mlango wa Isiraeli: Ameanguka, hatainuka tena mwanamwali wa Isiraeli, amebwagwa, alale juu ya nchi yake, hakuna atakayemwinua. Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mji unaopeleka elfu vitani utasaza mia tu, nao unaopeleka mia utasaza kumi tu kwao walio mlango wa Isiraeli. Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyowaambia walio mlango wa Isiraeli: Nitafuteni! Ndipo, mtakapopona. Lakini msinitafute huko Beteli! Wala msije kuingia Gilgali! Wala msiondoke kwenda Beri-Seba! Kwani Gilgali utatekwa na kuhamishwa, nao Beteli utageuka kuwa si kitu. Mtafuteni Bwana! Ndipo, mtakapopona. Asiujie mlango wa Yosefu kama moto utakaouteketeza, kwa kuwa Beteli hakuna atakayeweza kuuzima. Mashauri yapasayo mnayageuza kuwa uchungu, nayo yaongokayo mnayakanyaga uvumbini. Yeye ndiye aliyezifanya nyota, zile za Kilimia nazo zake Choma, nikuchome! Yeye ndiye anayeigeuza giza kuwa mapema, tena mwanga wa mchana huugeuza kuwa giza ya usiku! Yeye ndiye anayeyaita maji ya bahari, akayafurikisha juu ya nchi! Bwana ni Jina lake. Yeye ndiye anayewaletea wanguvu mwangamizo, uwatokee kama umeme, nayo miji yenye maboma ya nguvu iingiliwe na mwangamizo. Wao humchukia ayakataye mashauri ya langoni sawasawa, naye asemaye ya kweli huwachafua mioyo. Kwa kuwa mnamkanyaga mnyonge, mkamtoza kodi ya ngano, mmepata kujijengea nyumba za mawe ya kuchonga, lakini hamtakaa ndani yao; mkajipandia mashamba mazuri ya mizabibu, lakini hamtazinywa mvinyo zao. Kwani ninayajua mapotovu yenu yaliyo mengi nayo makosa yenu yanayozidi. Mnamsonga aliye mwongofu mkitaka kupenyezewa, mkawapotoa maskini, wasishinde shaurini. Kwa hiyo aliye mwenye akili hunyamaza siku hizi, kwani siku hizi ni mbaya kweli. Yatafuteni yaliyo mema mkiyaacha yaliyo mabaya, mpate kupona! Ndipo, Bwana Mungu Mwenye vikosi atakapokuwa nanyi, kama mlivyosema wenyewe. Yachukieni yaliyo mabaya! Yapendeni yaliyo mema! Simamisheni langoni mashauri yaliyo sawa! Ndipo, Bwana Mungu Mwenye vikosi atakapowahurumia walio masao yake Yosefu. Kweli Bwana Mungu Mwenye vikosi, yeye Bwana anasema hivi: Katika viwanja vyote yatakuwako maombolezo, napo barabarani po pote watalia kwamba: Hoi! Hoi! Mkulima watamwita shambani, aje kuingia matanga, nao wajuao maombolezo watawaita, waje kuwalilia. Katika mashamba yote ya mizabibu yatakuwako maombolezo, kwani nitapita kwako katikati; ndivyo, Bwana anavyosema. Yatawapata wanaoitamani siku ya Bwana! Ninyi siku ya Bwana itawafaliaje? Ndiyo giza, siyo mwanga. Itakuwa, kama mtu akimkimbia simba, akaja kukutana na chui, au kama mtu akiingia nyumbani, akauegemeza mkono wake ukutani, kisha akatokea nyoka, akamwuma. Je? Siku ya Bwana siyo giza? Ndio, haina mwanga; ni yenye weusi, hauangazi kabisa. nimechukizwa na sikukuu zenu, sizitaki; wala mnuko wa mikutano yenu ya kunitambikia usinijie! Ingawa mnitolee ng'ombe za kuteketezwa nzima pamoja na vipaji vyenu vya tambiko, sitapendezwa, wala vinono vyenu vya kunishukuru sitavitazama. Iondoe kwangu milio ya nyimbo zako! Nazo sauti za mapango yako sitaki kuzisikia. Lakini mashauri yaliyo sawa na yaendelee kama maji, nayo yaongokayo na yawe kama mto usiokupwa! Je? Ng'ombe na vipaji, mlivyovitoa nyikani miaka arobaini, vilikuwa vya kunitambikia mimi, ninyi mlio mlango wa Isiraeli? Kwa kuwa mlimchukua Sikuti, awe mfalme wenu, navyo vinyua vyenu vya Kiyuni, mlivyojifanyizia wenyewe, viwe nyota zake mungu wenu: basi, kwa hiyo nitawahimisha, mwende mbali kuliko Damasko. Ndivyo, Bwana anavyosema; Mungu Mwenye vikosi ni Jina lake. Yatawapata watuliao Sioni nao wajivuniao mlima wa Samaria, ndio wakuu wa taifa lililo la kwanza, nao walio mlango wa Isiraeli huwaendea! Haya! Nendeni Kalne, mkatazame! Tena tokeni huko kwenda Hamati ulio mji mkuu! Kisha shukeni Gati kwa Wafilisti, mwone! Je? Ninyi m wema kuliko watu wa nchi hizo za kifalme? Je? Mipaka yao siyo mikubwa kuliko mipaka yenu? Siku mbaya mnaiwazia kuwa mbali bado, lakini kao la makorofi mnalileta kuwa karibu. Ninyi hulalia vitanda vya pembe za tembo na kujinyosha katika magodoro yenu mororo! Hula wana kondoo mkiwatoa makundini, nao ndama mkiwatoa mazizini! Hujipigia mapango, tena hujitungia vinanda vinginevyo kama Dawidi. Hunywa mvinyo katika mabakuli, tena hujipaka marashi yapitayo yote; lakini hivyo, Yosefu alivyovunjwa, haviwaumizi. Kwa hiyo watatekwa sasa na kuhamishwa, waende mbele ya mateka; ndipo, yatakapokomea makelele ya michezo yao waliojinyosha hivyo. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Mwenye vikosi: Bwana Mungu ameapa rohoni mwake kwamba: Majivuno ya Yakobo hunitapisha, nikachukizwa na majumba yake, kwa sababu hii nitautoa huo mji pamoja nayo yote yaliyomo mwake. Itakuwa, waume kumi watakaposazwa katika nyumba moja, watakufa. Ndugu ya mtu apaswaye na kumteketeza mwenziwe akimchukua, aitoe mifupa yake nyumbani, kama anamwuliza aliomo nyumbani ndani: Yumo, uliye naye humu? atamjibu: Wamekwisha kufa! Ndipo, atakapomwambia: Nyamaza kimya! Kwani haifai kulikumbusha Jina la Bwana. Kwani mtaona: Bwana akiagiza, ndipo, watakapozipiga nyumba kubwa, hata zibomoke, nazo nyumba ndogo, hata ziatuke nyufa. Je? Farasi hupiga mbio mwambani? Au mtu atapalima na ng'ombe? Kwani mashauri yaliyo sawa mmeyapotoa, yawe maji ya nyongo, nayo yaliyotengenezwa, yaongoke, mmeyapotoa, yawe uchungu. Mwafurahia kisicho kitu na kusema: Hatukujipatia pembe kwa uwezo wetu sisi? Kwa hiyo ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Mwenye vikosi: Mtaniona, nikiwainulia taifa ninyi mlio mlango wa Isiraeli; ndio, watakaowasonga ninyi kuanzia penye njia ya kwenda Hamati, kufikisha penye mto wa nyikani. Haya ndiyo maono, Bwana Mungu aliyonionyesha: Nimemwona, alivyotengeneza nzige hapo, mimea ya vuli ilipoanza kuchipuka; nayo ilikuwa ya majani ya vuli iliyochipuka, watu walipokwisha kumkatia mfalme majani ya ng'ombe. Ikawa, nzige walipokwisha kula majani ya nchi, nikasema: Bwana Mungu, waachilie! Yakobo atawezaje kusimama? Kwani yeye ni mdogo. Ndipo, Bwana Mungu alipoigeuza roho kwa ajili ya hayo naye Bwana akasema: Hayatakuwa. Hili ndilo ono, Bwana Mungu alilonionyesha: Nimeona, Bwana Mungu alivyouita moto kuja kumgombea. Nao ukala vilindi vikubwa vya maji, ukataka kula napo pa kulimia. Ndipo, niliposema: Bwana Mungu, acha hapo! Yakobo atawezaje kusimama? Kwani yeye ni mdogo. Ndipo, Bwana alipoigeuza roho kwa ajili ya hayo, naye Bwana Mungu akasema: Haya nayo hayatakuwa. Hili ndilo ono, alilonionyesha: Nimemwona Bwana Mungu, alivyosimama juu ya ukuta uliosimama sawasawa kwa kujengwa kwa kipimo cha timazi, naye alishika kipimo cha timazi mkononi mwake. Bwana akaniuliza: Unaona nini, Amosi? Nilipojibu: Kipimo cha timazi, Bwana akaniambia: Utaniona, nitakavyowapima walio ukoo wangu wa Isiraeli, sitaendelea tena kuwapita tu. Vilima vya Isaka vitaangamizwa, napo patakatifu pote pa Isiraeli patabomolewa, nami nitawainukia walio mlango wa Yoroboamu kwa upanga. Ndipo, Amasia, mtambikaji wa Beteli, alipotuma kwa Yoroboamu, mfalme wa Isiraeli, kumwambia: Amosi anakuvurugia watu humu katika mlango wa Isiraeli, nchi haiwezi tena kuyavumilia maneno yake yote. Kwani haya ndiyo, Amosi anayoyasema: Yoroboamu atakufa kwa upanga, nao Waisiraeli watatekwa na kuhamishwa, watoke katika nchi yao. Kisha Amasia akamwambia Amosi: Wewe mchunguzaji, nenda zako kukimbia katika nchi ya Yuda, ukajilie mkate huko na kuwafumbulia maneno! Lakini huku Beteli usitufumbulie tena maneno, kwani hapa ndipo patakatifu pa mfalme, nayo nyumba hii ni ya ufalme wote. Amosi akamjibu Amasia na kumwambia: Mimi si mfumbuaji wala mwana wa mfumbuaji, kwani nalikuwa mchunga ng'ombe, nikajitunzia mikuyu. Ndipo, Bwana aliponichukua, akanitoa penye ng'ombe, Bwana akaniambia: Nenda, uwafumbulie walio ukoo wangu wa Isiraeli! Sasa lisikie neno la Bwana! Wewe unasema: Usiwafumbulie Waisiraeli! Wala usiwahubiri walio mlango wa Isaka yatakayokuwa! Ni kwa sababu hii, Bwana akisema hivyo: Mkeo atakuwa mgoni humu mjini, nao wanao wa kiume na wa kike watauawa kwa upanga, nalo fungu lako la nchi litagawanywa kwa kupimwa na kamba. Nawe wewe utakufa katika nchi iliyo na mwiko wa kuikaa, nao Waisiraeli watatekwa na kuhamishwa, watoke katika nchi yao. Hili ndilo ono, Bwana Mungu alilonionyesha: Nimeona kikapu chenye matunda yaliyoiva. Akaniuliza: Unaona nini, Amosi? Niliposema: Kikapu chenye matunda yaliyoiva, Bwana akaniambia: Zimetimia siku za kuishia kwao walio ukoo wangu wa Isiraeli, sitaendelea tena kuwapita tu. Siku hiyo ndipo, nyimbo za majumbani zitakapokuwa vilio, kwani mizoga ya watu itakuwa mingi, mahali po pote wataitupa tu na kunyamaza kimya; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Lisikieni hili, ninyi mfokeao maskini, mkakanyaga wanyonge wa nchi Mwasema: Mwezi mpya utatokea lini, tupate kuuza ngano? Nayo siku ya mapumziko itapita lini, tupate kufungua malimbikio? Ndipo, tutakapopunguza pishi pamoja na kuongeza bei, tuwadanganye watu kwa mizani zilizo za uwongo. Ndipo, tutakaponunua wanyonge kwa fedha, wawe watumwa, nao maskini kwa viatu viwili, makumvi ya ngano nayo tutayauza. Bwana ameapa na kumtaja aliye mkuu wa Yakobo kwamba: Sitayasahau kale na kale matendo yao yote! Je? Kwa ajili ya hayo nchi isitetemeke? Asiomboleze kila mtu akaaye huku? Nchi yote nzima itajitutumua kama mto wa Nili kwa kuchafuka, kisha itakupwa kama lile jito la Misri. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Siku hiyo ndipo, nitakapoliendesha jua, lichwe mnamo saa sita, niugeuze mwanga wa mchana kuwa giza katika nchi. Nazo sikukuu zenu nitazigeuza kuwa za maombolezo, nazo nyimbo zenu zote kuwa vilio; kisha nitawavika nyote magunia viunoni, napo vichwani penu nyote nitatoa vipara. Nitafanya, maombolezo yawe kama ya kumwombolezea mwana wa pekee, mwisho wao uwe kama siku yenye uchungu. *Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Mtaona, siku zikija, nitakapotuma njaa, ije kuingia katika nchi hii, siyo njaa ya chakula, wala siyo kiu ya maji, ila itakuwa njaa ya kuyasikia maneno ya Bwana. Ndipo, watakapotangatanga, watoke baharini, wafike kwenye bahari nyingine, tena watoke upande wa kaskazini, wafike upande wa maawioni kwa jua; watazunguka po pote kwa kulitafuta Neno la Bwana, lakini hawataliona.* Siku hiyo ndipo, watakapozimia kwa kiu wanawali wazuri pamoja na wavulana. Ndio wao wanaoapa na kuvitaja vinyua vya Samaria vinavyowakosesha, nao wasemao: Hivyo, Mungu wako, Dani, alivyo mzima! Au: Hivyo, njia ya Beri-Seba inavyotupa uzima! wataanguka, lakini hawatainuka tena. Nimemwona Bwana, akisimama penye kutambikia na kusema: Zipige nguzo pembeni juu, vizingiti vya juu vitikisike! Kisha uviponde, viwaangukie vichwani pao wote! nao watakaosalia nitawaua kwa upanga, pasiwe hata mmoja kwao, atakayekimbia, wala mmoja wao atakayepona. Ingawa wapenyelee kuzimuni, huko nako mkono wangu utawatoa; ingawa wapande mbinguni, huko nako nitawabwaga chini. Ingawa wajifiche mlimani kwa Karmeli juu, huko nako nitawakamata na kuwachukua; ingawa wajitoweshe machoni pangu baharini chini kabisa, huko nako nitawaagizia nyoka, awaume. Ingawa waje mbele ya adui zao wakihamishwa kwenda utumwani, huko nako nitawaagizia upanga, uwaue; ndipo, nitakapowaelekezea macho yangu, niwapatie mabaya, nisiwapatie mema. Hapo, Bwana Mungu Mwenye vikosi atakapoigusa nchi, itayeyuka papo hapo, wote wakaao huko waomboleze; ndipo, nchi yote itakapojitutumua kama mto wa Nili, kisha itakupwa kama lile jito la Misri. Ndiye aliyepajenga pake mbinguni kuwa dari yake, nayo misingi ya kao lake aliiweka chini; ndiye anayeyaita maji ya baharini, ayafurikishe juu ya nchi kavu. Bwana ni Jina lake! Ndivyo, yeye Bwana asemavyo: Ham sawasawa kama wana wa Kinubi, ninyi wana wa Isiraeli? Waisiraeli sikuwatoa katika nchi ya Misri? Nao Wafilisti kule Kafutori? Nao Washami kule Kiri? Mtaona, macho yangu Bwana Mungu yakiutazama ufalme uliokosa niutoweshe juu ya nchi, lakini sitautowesha mlango wa Yakobo wote mzima; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani mtaona, nikitoa amri, niwapepete walio mlango wa Isiraeli na kuwatapanya kwa mataifa yote, kama ngano zinavyopepetwa katika ungo, pasipatikane hata chembe moja itakayoanguka chini. Wakosaji tu wa ukoo wangu watauawa wote kwa panga, ndio waliosema: Mabaya hayatatufikia, wala hayatatupata. Siku hiyo ndipo, nitakapokisimamisha kibanda cha Dawidi kilichoanguka, na kuziziba nyufa zake na kuyasimamisha mabomoko yake, nikijenge, kiwe kama siku za kale, wayatwae masao ya Edomu na wamizimu wote waliotangaziwa Jina langu; ndivyo, asemavyo Bwana, naye atayafanya haya. Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, mwenye kulima atakaposhikamana na mvunaji, vile vile mwenye kuzikamua zabibu na mpanda mbegu. Ndipo, milima itakapochuruzika pombe mbichi, vilima vyote vifurikwe nazo. Ndipo, nitakapoyafungua mafungo yao walio ukoo wangu wa Isiraeli, waijenge miji yao iliyoangamizwa, waipande mizabibu yao, wapate kunywa mvinyo zao. Ndipo, nitakapowapanda katika nchi yao, wasing'olewe tena katika nchi yao, niliyowapa. Bwana Mungu wako ameyasema. Ndivyo, Bwana Mungu anavyosema kwa ajili ya Edomu: Tumesikia mbiu kwake Bwana, ya kuwa mjumbe ametumwa kwenda kwa mataifa kwamba: Ondokeni! Na tuondoke kwenda kupigana naye! Utaniona, nikikufanya kuwa mdogo katika mataifa, ubezwe kabisa wewe! Majivuno ya moyo wako yamekudanganya ukaaye nyufani kwenye miamba katika makao yaliyoko huko juu, ukasema moyoni mwako: Yuko nani atakayenibwaga chini? Lakini ijapo uvijenge vituo vyako juu kabisa kama tai, ijapo utue katikati ya nyota, huko nako nitakubwaga chini; ndivyo, asemavyo Bwana. Kama wezi wangekujia, au kama waangamizaji wangekujia usiku, wasingeiba tu, mpaka wakitoshewa? Lakini nawe ungekuwa umeangamizwa kabisa. Kama wachuma zabibu wangekujia, Lakini tazameni, mali za Esau zilivyotafutwa zote, malimbiko yake nayo yalivyochunguzwa! Wote, uliofanya maagano nao, wamekukimbiza hata mipakani; wote, uliopatana nao, wamekudanganya, wakakushinda, waliokula chakula chako wamekutegea matanzi chini, lakini mwenyewe huyatambui maana. Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku hiyo, nitakapowapoteza werevu wa kweli kwake Edomu, sipo, utambuzi nao utakapopotea milimani kwa Esau? Ndipo, mafundi wenu wa vita, ninyi Watemani, watakapokata tamaa, kusudi kila mmoja ang'olewe milimani kwa Esau kwa kuuawa. Kwa hivyo, ulivyomkorofisha ndugu yako Yakobo, soni zitakufunika, mpaka uangamie kale na kale. Kwani walisimama upande mwingine siku ile, wengine walipoziteka mali zake, wageni walipoingia malangoni mwake na kuupigia Yerusalemu kura, ndipo, wewe nawe ulipokuwa kama mwenzao wao hao. Lakini usimwonee ndugu yako, akipatwa na siku mbaya, siku ikiwa ya kuona mambo mageni! Wala usiwafurahie wana wa Yuda siku, wakiangamia! Wala usiwe na madomo makubwa siku, wakisongeka! Wala usiingie malangoni mwao walio ukoo wangu siku, wakiteseka! Wala usiwaonee nawe, wakipatwa na mabaya siku, wakiteseka! Wala usiinyoshe mikono yako kukamata mali zao siku, wakiteseka! Wala usisimame penye njia panda kuwaua watu wao waliokimbia! Wala masao yao usiwatie mikononi mwa adui siku, wakisongeka! Kwani siku ya Bwana iko karibu, iwajie wao wa mataifa yote; ndipo, utakapofanyiziwa, kama ulivyofanya, matendo yako yakikurudia kichwani pako. Kwani kama ulivyokunywa katika mlima wangu mtakatifu, ndivyo, mataifa yote watakavyokunywa pasipo kukoma, watakunywa na kumeza vibaya, wawe kama watu wasiokuwapo kabisa. Lakini mlimani pa Sioni watakuwapo waliojiponya, napo patakuwa Patakatifu. Nao walio mlango wa Yakobo watakuwa moto, nao walio mlango wa Yosefu watakuwa miali ya moto, lakini walio wa mlango wa Esau watakuwa majani makavu, ndiyo watakayoyawasha na kuyala. Kwa hiyo hawatakuwapo walio masao ya Esau, kwani Bwana ameyasema. Nao wakaao upande wa kusini wataitwaa milima ya Esau, nao wakaao mrimani wataitwaa nchi ya Wafilisti, nayo mashamba ya Efuraimu nayo mashamba ya Samaria watayatwaa, nao Wabenyamini watatwaa Gileadi. Navyo vikosi vya wana wa Isiraeli waliotekwa na kuhamishwa ndio watakaoitwaa nchi ya Kanaani mpaka Sareputa, nao Wayerusalemu waliotekwa na kuhamishwa Sefaradi wataitwaa miji iliyoko upande wa kusini. Kisha waokozi wataupanda mlima wa Sioni, waipatilize milima ya Esau; lakini ufalme utakuwa wake Bwana. Neno la Bwana likamjia Yona, mwana wa Amitai, kwamba: Ondoka, uende katika mji ule mkubwa wa Niniwe, uutangazie, ya kuwa ubaya wao umenitokea hapa juu! Lakini Yona akaondoka kumkimbia Bwana, aende Tarsisi, akatelemka kwenda Yafo; ndipo, alipoona merikebu inayokwenda Tarsisi, akawapa nauli yao, akajipakia mle kwenda nao Tarsisi, amkimbie Bwana. Ndipo, Bwana alipotuma upepo mkali huko baharini, ukawa kimbunga kikali kule baharini, ile merikebu ikawa karibu ya kuvunjika. Mabaharia wakaogopa, wakaililia miungu, kila mtu mungu wake, kisha vyombo vilivyokuwamo merikebuni wakavitupa baharini, merikebu ipate kuwa nyepesi. Lakini Yona alikuwa ameshuka na kuingia chumba cha ndani cha huko chini, akalala usingizi mwingi. Mkuu wa merikebu akamjia, akamwambia: Inakuwaje ukijilalia usingizi? Inuka, umlilie Mungu wako! Labda Mungu atatukumbuka, tusiangamie. Kisha wote wakaambiana, kila mtu na mwenziwe: Haya! Na tupige kura, tujue, kama ni kwa ajili ya nani, tukipatwa na mabaya haya! Walipopiga kura, ikamwangukia Yona. Wakamwambia: Tuelezee, kama ni kwa sababu gani, tukipatwa na mabaya haya! Unafanya kazi gani? Tena ni wapi, ulikotoka? Nchi yako ni ipi? U mtu wa kabila gani wewe? Akawaambia: Mimi ni Mwebureo, mimi ninamcha Bwana, Mungu wa mbingu, aliyezifanya bahari na nchi kavu. Ndipo, wale waume waliposhikwa na woga mwingi, wakamwuliza: Umefanya nini? Kwani waume wale walikwisha jua, ya kuwa amemkimbia Bwana, kwani aliwasimulia. Wakamwuliza: Tukufanyie nini, bahari ipate kutulia mbele yetu? Kwani bahari ilikuwa ikiendelea kuchafuka zaidi. Akawaambia: Nichukueni mnitupe baharini! Ndipo, bahari itakapotulia mbele yenu, kwani ninajua, ya kuwa ni kwa ajili yangu mimi, hiki kimbunga kikubwa kikiwatokea ninyi. Kisha wale waume wakafanya bidii sana kuvuta makasia, wapeleke merikebu pwani, lakini hawakuweza, kwani bahari ilikuwa ikiendelea kuwachafukia zaidi. Ndipo, walipomlilia Bwana kwamba: E Bwana, usiache, tukiangamia kwa ajili ya roho ya mtu huyu! Wala usitutwike damu, tusiyoikosea! Kwani wewe Bwana umefanya, kama ulivyopendezwa. Kisha wakamchukua Yona, wakamtupa baharini; ndipo, bahari ilipotulia ikiacha kuchafuka. Kwa hiyo wale waume wakamwogopa Bwana, woga mwingi ukawashika, wakamtambikia Bwana na kumtolea ng'ombe ya tambiko pamoja na kumwapia viapo. Bwana akaagiza samaki mkubwa, aje ammeze Yona, Yona akawamo tumboni mwa samaki huyo siku tatu mchana na usiku. Mle tumboni mwa huyo samaki Yona akamwomba Bwana Mungu wake kwamba: Nimemlilia Bwana niliposongeka, akaniitikia; kuzimuni ndani nimemlalamikia, aniokoe, ndipo, alipoisikia sauti yangu. Umenitupa vilindini baharini ndani, mafuriko ya maji yanizunguke, mawimbi yako yote na maumuko yako yote yakapita juu yangu. Nami nikawaza kwamba: Nimetupwa, nisitokee tena machoni pako, nitawezaje kuliona tena Jumba lako takatifu? Maji yamenizunguka ya kuitosa nayo roho yangu, vilindi vimenizunguka, majani ya baharini yamekizinga kichwa changu. Nimezama kuifikia misingi ya milima, makomeo ya nchi yamenifungia kale na kale, lakini wewe Bwana Mungu wangu umenitoa kuzimuni, niwe mzima. Roho yangu ilipokuwa katika kuzimia ndani yangu, ndipo, nilipomkumbuka Bwana, maombo yangu yakakufikia katika Jumba lako takatifu. Washikao mizimu iliyo ya uwongo tu humwacha awahurumiaye, lakini mimi nitapaza sauti za kukushukuru, ziwe ng'ombe zangu za tambiko, nitakazokutolea, nayo, niliyokuapia na niyalipe! Wokovu uko kwake Bwana. Ndipo, Bwana alipomwagiza yule samaki, naye akaja kumtapika Yona pwani. Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili kwamba: Ondoka, uende katika mji ule mkubwa wa Niniwe, uutangazie utume, nitakaokuambia! Ndipo, Yona alipoondoka, akaenda Niniwe, kama Bwana alivyomwagiza. Niniwe ulikuwa mji mkubwa machoni pa Mungu; kuupita kati ulikuwa mwendo wa siku tatu. Yona akaanza kuingia mjini mwendo wa siku moja, akapiga mbiu kwamba: Zingaliko siku 40; zitakapopita, mji wa Niniwe utabomolewa. Ndipo, watu wa Niniwe walipomtegemea Mungu, wakatangaza, watu wafunge mfungo, wakavaa magunia wote, wakubwa mpaka wadogo. Habari ya mambo hayo ikafika hata kwa mfalme wa Niniwe, naye akaondoka katika kiti chake cha kifalme, akalivua vazi lake la kifalme, akavaa gunia, akajikalisha majivuni. Kisha akatangaza mbiu mle Niniwe ya kwamba: Kwa amri ya mfalme na ya wakuu wake yanaagizwa haya: Watu na nyama, kama ni ng'ombe au kondoo, wasionje kitu cho chote, wasile, wala maji tu wasinywe! Ila wajivike magunia, watu nao nyama, wakaze kumlilia Mungu! Kisha kila mtu arudi katika njia yake mbaya na kuyaacha makorofi yaliyomo mikononi mwake! Labda ndivyo, Mungu atakavyogeuza moyo, ayaache makali yake yenye moto, tusiangamie. Mungu alipoyaona matendo yao, ya kuwa wamerudi katika njia zao mbaya, ndipo, Mungu alipogeuza moyo, akaacha kuyafanya yale mabaya, aliyoyasema, ya kuwa atawafanyizia; hakuyafanya. Hivi vikamkasirisha Yona sana na kumchafua moyo wake, akamwomba Bwana kwamba: E Bwana, haya siyo, niliyoyasema nilipokuwa katika nchi ya kwetu? Kwa hiyo naliondoka kukimbilia Tarsisi, kwani nalijua, ya kuwa wewe ndiwe Mungu mwenye utu na huruma, tena u mwenye uvumilivu na upole mwingi, hugeuza moyo, usifanye mabaya. Sasa, Bwana, jitwalie roho yangu, initoke! Kwani kufa kwangu ni kwema kuliko kuishi. Bwana akamjibu: Je? Ni vema ukichafuka hivyo? Kisha Yona akatoka mle mjini, akakaa nje ya mji upande wa maawioni kwa jua, akajijengea kibanda kidogo, akakaa chini yake kivulini, mpaka aone, mambo ya mji yatakavyokuwa. Bwana Mungu akaagiza mbonobono, akauotesha, uwe juu ya mahali pake Yona, umpatie kivuli cha kichwa chake, uondoe hivyo ubaya moyoni mwake. Yona akaufurahia sana huo mbonobono. Lakini kulipopambazuka siku ya kesho kutwa, Mungu akaagiza kidudu, kikautoboa huo mbonobono, ukanyauka. Ikawa, jua lilipopanda juu, Mungu akaagiza upepo wenye joto utokao upande wa maawioni kwa jua; basi, jua lilipompiga Yona kichwani, akazimia, akajitakia kufa akisema: Kufa kwangu ni kwema kuliko kuishi. Mungu akamwambia Yona: Je? Ni vema, ukichafuka hivyo kwa ajili ya mbonobono? Akajibu: Ndio, ni vema, nikikasirika, mpaka nife. Bwana akamwambia: Wewe unauonea mbonobono huu uchungu, tena hukuusumbukia, wala hukuukuza; uliota na usiku, tena umekufa na usiku mwingine. Nami nisiuonee uchungu mji huu mkubwa wa Niniwe, kwa kuwa humu wamo watu kupita 120000 wasiojua kupambanua yaliyoko kuumeni nayo yaliyoko kushotoni? Tena wamo nyama wengi. Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Mika wa Moreseti siku zile, Yotamu na Ahazi na Hizikia walipokuwa wafalme wa Yuda, ni ono lake la mambo yatakayoijia miji ya Samaria na ya Yerusalemu. Sikieni, ninyi makabila yote! Sikilizeni, nchi nao wote walioko! Bwana Mungu na atoe ushahidi wa kuwashinda ninyi akitokea katika Jumba lake takatifu. Kwani mtamwona Bwana, akiondoka mahali pake, akishuka akikanyaga juu ya vilima vya nchi. Ndipo, milima itakapoyeyuka chini yake, nayo mabonde yataatuka nyufa; itayeyuka kama nta motoni, iwe kama maji yaporomokayo magengeni. Hayo yote yatakuja kwa ajili ya upotovu wa Yakobo, na kwa ajili ya makosa yao walio mlango wa Isiraeli. Upotovu wa Yakobo ndio nini? Sio ule wa Samaria? Napo pa kutambikia vilimani ndipo wapi? Sipo Yerusalemu? Kwa hiyo nitaugeuza Samaria, uwe chungu la mawe shambani pa kupandia mizabibu, nayo mawe yake nitayaporomosha bondeni, niifunue misingi yake, iwe wazi. Vinyago vyao vyote vya kuchonga vitakatwakatwa, nayo mishahara ya ugoni itateketezwa kwa moto; vinyago vyao vyote pia nitavitoa, viharibiwe, kwani wamevipata vyote kuwa mshahara wa ugoni, navyo vitakuwa mshahara wa ugoni tena. Hayo ndiyo, ninayotaka kuyaombolezea na kupiga vilio nikitembea pasipo nguo kuwa mwenye uchi kabisa, nifanye maombolezo kama mbweha na kupiga vilio kama wana wa mbuni. Kwani mapigo yako hayaponi, yatamfikia naye Yuda, yatagonga hata malangoni kwao, walio ukoo wangu, mle malangoni mwa Yerusalemu. Msiyasimulie Gati (Penye Masimulio), msilie kabisa! Gaagaeni uvumbini Beti-Leafura (Nyumba ya Uvumbi)! Jiendeeni mkaao Safiri (Mji wa Mapambo) na kuona soni kwa kuwa wenye uchi! Wakaao Sanani (Matokeo) hawatoki tena, maombolezo ya Beti-Haeseli (Nyumba ya Wanyimaji) yatawanyima fikio. Wakaao Maroti (Uchungu) wanaona uchungu kwa ajili ya mema yao, kwani mabaya yameyashukia malango ya Yerusalemu toka kwa Bwana. Gari la vita lifungie farasi wenye mbio, ukaaye Lakisi (Panapopigwa Mbio)! Kwani huko ndiko, binti Sioni alikoanzia kukosa, kwani kwao ndiko, mapotovu ya Isiraeli yalikoonekana. Kwa hiyo huna budi kutoa vipaji vya kuachana, uwape wa Moreseti-Gati (Uchumba wa Gati). Nyumba za Akizibu (Madanganyo) zitawadanganya wafalme wa Isiraeli. Ninyi mkaao Maresa (Wenyeji) nitawaletea mwenyeji wa kweli, utukufu wa Isiraeli utajiendea mpaka Adulamu. Jikatie nywele, uwe mwenye kipara kwa ajili ya watoto wako waliokupendeza! Kikuze sana kipara chako, kiwe kama cha ngusu, kwani wametekwa na kuhamishwa kwako. Yatawapata wanaowaza maovu, watungao mabaya vitandani mwao, wayafanye asubuhi kutakapopambazuka, mikono yao ikiweza kuyamaliza. Kwa kutamani mashamba huyanyang'anya; ikiwa nyumba, huzichukua nazo, humkorofisha mwenye nyumba pamoja nao waliomo, vilevile mwenye shamba, ijapo liwe fungu lake. Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtayaona mabaya, ninayouwazia mlango huu! Yakiwapata, hamtaweza kuzitoa shingo zenu mle, wala hamtaweza kwenda na kuzinyosha shingo zenu, kwani siku hizo zitakuwa mbaya kweli. Siku hiyo watawatungia ninyi mfano, wataomboleza ombolezo la kwamba: Imefanyika! Tumeangamizwa! Mafungu yao walio ukoo wangu anawapa wengine! Kumbe mimi ameninyang'anya mashamba yetu, awagawie wao wamkataao! Kwa hiyo hamtapata tena katika mkutano wa Bwana atakayempimia mtu fungu, alilolipata kwa kura. Wao huhubiri: Msihubiri! Haifai kuhubiri mambo kama hayo, matusi nayo hayakomi! Je? Sio walio mlango wa Yakobo wanaosema: Inakuwaje? Roho yake Bwana ni nyepesi ya kukasirika? Au matendo yake ni yayo hayo? Hasemi: Ninamwendea kwa wema ashikaye njia inyokayo? Lakini tangu kale mmewainukia walio ukoo wangu, kama ni adui zenu; wapitao pasipo mawazo mabaya mwawavua kanzu za juu na mavazi ya ndani, kama ni mateka ya vitani. Wanawake wao walio ukoo wangu mwawafukuza katika nyumba zao zilizowapendeza, watoto wachanga wao mkawanyang'anya utukufu wangu, wasiupate kale na kale. Kwa hiyo: Ondokeni! Nendeni! Kwani huku hakuna pa kutulia kwa ajili ya uchafu unaowaangamiza, mwangamie kabisa kabisa. Kama angekuja mtu anayegeukageuka kama upepo, anayedanganya watu kwa kuwaongopea, kama angesema: Nitawahubiri mambo ya mvinyo na ya vileo, basi, yeye angekuwa mhubiri, watu hawa wanayemtaka. Kweli nitawaokota nyote pia mlio wa Yakobo; kweli nitawakusanya mlio masao ya Isiraeli, niwaweke pamoja zizini kama kondoo, wawe kama kundi la kondoo walioko katikati ya malisho yao, wafanye mtutumo kwa kuwa watu wengi. Mwenye kuwavunjia njia atawatangulia, wapite langoni kwa kupavunja, watoke nje papo hapo; ndipo, mfalme wao atakapowaongoza, lakini atakayekwenda mbele yao wote ni Bwana. Nikasema: Sikilizeni, ninyi mlio vichwa vyao wa Yakobo, ninyi mlio wakuu wa mlango wa Isiraeli! Je? Haiwapasi ninyi kujua, jinsi mashauri yanavyokatwa sawasawa? Lakini ninyi huchukizwa nayo yaliyo mema, mkapendezwa nayo yaliyo mabaya; ninyi huchuna watu ngozi zao, nazo nyama zao huziondoa mifupani kwao. Ninyi ndio mnaozila nyama zao walio ukoo wangu, tena mkiisha kuwavua ngozi zao mwawavunja nayo mifupa yao, mkawakatakata vipande kama vya kuweka chunguni au kama nyama zinazotiwa katika sufuria. Kwa hiyo hapo, watakapomlilia Bwana, hatawaitikia, ila atauficha uso wake, usiwatazame wakati huo, kama inavyowapasa kwa matendo yao mabaya, waliyoyafanya. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya wafumbuaji wanaowapoteza walio ukoo wangu, ndio wanaotangaza kwamba: Tengemaneni tu! wakipata vya kutafuna kwa meno yao, lakini mtu asipowapa vya kutia vinywani mwao, humpatia vita vya watakatifu Kwa hiyo usiku utawaguia, msione kitu, na giza, msiweze kuagua, nalo jua litawachwea wafumbuaji hao, hata siku itakuwa yenye giza kwao. Ndipo, hao wachunguzaji watakapopatwa na soni, nao waaguaji hao wataiva nyuso, wao wote watajifunika ndevu zao za midomo, kwa kuwa Mungu hawajibu kamwe. Lakini mimi nimejaa nguvu, nilizopewa na Roho ya Bwana, nikapewa kumaliza mashauri kwa uwezo wa kushinda, nipate kuwatangazia wa Yakobo mapotovu yao nao Waisiraeli makosa yao. Sikilizeni, ninyi mlio vichwa vyao wa Yakobo, nanyi mlio waamuzi wa mlango wa Isiraeli! Mwachukizwa na mashauri yaliyo sawa, nayo yote yanyokayo mwayapotoa! Sioni mwaujenga kwa damu nao Yerusalemu kwa mapotovu. Wakuu wao hukata mashauri kwa kupenyezewa mali, nao watambikaji wao hufundisha kulipwa, nao wafumbuaji wao hufumbua kwa kupata fedha, tena hujiegemezea kwake Bwana na kusema: Je? Bwana hayuko kwetu katikati? Hakuna kibaya kitakachotupata. Kweli kwa ajili yenu ninyi Sioni utalimwa kuwa shamba, nao Yerusalemu utageuka kuwa chungu la mabomoko, nao mlima wenye Nyumba hii utageuka kuwa kilima chenye mwitu. Mwisho wa siku utakapotimia, mlima wenye Nyumba ya Bwana utakuwa umeshikizwa na nguvu, uwe wa kwanza wa milima, uende juu kuliko vilima vingine; ndiko, makabila ya watu watakakokimbilia. Nao wamizimu wengi watakwenda huko wakisema: Njoni, tupande mlimani kwa Bwana kwenye Nyumba ya Mungu wa Yakobo! Atufundishe, njia zake zilivyo, tupate kwenda na kuifuata mikondo yake! Kwani Maonyo yatatoka Sioni, namo Yerusalemu mtatoka Neno lake Bwana. Ndipo, atakapoamulia makabila mengi na kuwapatiliza wamizimu wenye nguvu wakaao mbali; nao watazifua panga zao kuwa majembe, hata mikuki yao kuwa miundu, kwani hakuna taifa tena litakalochomolea jingine panga, wala hawatajifundisha tena mapigano ya vita. Watakaa kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mkuyu wake pasipo kuona atakayewastusha, kwani kinywa cha Bwana Mwenye vikosi kimeyasema. Kwani makabila yote kila moja hujiendea katika jina la mungu wake, lakini sisi tutakwenda kwa Jina la Bwana Mungu wetu siku zote kale na kale. Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku hiyo nitawaokota wachechemeao, niwakusanye waliotawanyika nao niliowafanyizia mabaya. Kisha nitawaweka wachechemeao kuwa masao, nao walioko mbali kuwa taifa lenye nguvu, naye Bwana atakuwa mfalme wao mlimani kwa Sioni toka sasa hata kale na kale. Nawe mnara wa kulindia makundi, wewe kilima cha binti Sioni, kwako wewe utarudi tena, ukufikie, ule utawalaji wa kwanza, ndio ufalme wa binti Yerusalemu. Mbona unapiga makelele sasa? Je? Mfalme hayumo mwako? Au ameangamia akuongozaye, uchungu ukikupata kama wa mwanamke anayezaa? Jipinde na kupiga kite kama mwanamke anayezaa, binti Sioni! Kwani sasa huna budi kutoka mjini, ukae porini, mpaka ufike Babeli; huko ndiko, Bwana atakakokuponya akikukomboa mikononi mwa adui zako. Lakini sasa wamizimu wengi watakukusanyikia wakisema: Sioni na uchafuliwe, macho yetu yaufurahie. Lakini wao hawayajui mawazo ya Bwana, wala hawalitambui shauri lake, ya kuwa ni yeye aliyewakusanya kama miganda penye kupuria. Inuka, binti Sioni, uwapure! Kwani pembe zako nitazigeuza kuwa chuma nayo kwato zako kuwa shaba, upate kuponda makabila mengi, umtolee Bwana mapato yao, yawe yake, nazo mali zao, ziwe zake yeye aliye Bwana wa nchi zote. Sasa jikusanyeni, wana wa mkutano! Kwani wametujengea boma, watusonge, naye mwamuzi wa Isiraeli wanampiga shavuni kwa fimbo. *Wewe Beti-Lehemu wa Efurata, ijapo uwe mdogo katika miji yenye maelfu ya Yuda, mwako ndimo, atakamonitokea yeye atakayekuwa mtawala Waisiraeli; matokeo yake ni ya siku nyingi za mbele, kweli ni ya siku za kale na kale. Kwa hiyo atawatoa, siku zitimie, yule atakayezaa atakapokuwa amezaa; ndipo, wazao wa ndugu zao watakaporudi kwao kwa wana wa Isiraeli. Ndipo, atakapotokea na kusimama, awachunge kwa nguvu za Bwana, kwa ukuu wa Jina la Bwana Mungu wake, nao watakaa, kwani hapo ndipo, atakapokua, awe mkuu mpaka mapeoni kwa nchi. Naye yeye atakuwa utengemano wetu.* Kama Waasuri wataingia katika nchi yetu, wakanyage namo majumbani mwetu, tutaweka wachungaji wetu saba, wawazuie, pamoja na watu wanane wa kifalme. Hao watailisha nchi ya Asuri kwa panga nayo nchi ya Nimurodi malangoni kwake. Ndivyo, atakavyotuponya mikononi mwa Waasuri, kama wanaingia katika nchi yetu na kukanyaga mipakani kwetu. Nao masao ya Isiraeli watakuwa kati ya makabila mengi kama umande utokao kwa Bwana, au kama manyunyu yanyeayo majani yasiyomngojea mtu, yasiyokalii wana wa watu. Kweli masao ya Yakobo watakuwa kwa wamizimu kati ya makabila mengi, kama simba alivyo katika nyama wa porini, au kama mwana wa simba alivyo katika makundi ya kondoo, akiwapita huwakanyaga pamoja na kuwararua, asipatikane mponya. Hivyo mkono wako utakuwa mkuu kwao wakusongao, nao adui zako watatoweshwa wote. Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku hiyo itakuwa, nitakapotowesha kwako farasi wako, nayo magari yako ya vita nitayapoteza. Nayo miji ya nchi yako nitaitowesha, nayo maboma yako yote nitayabomoa. Nazo hirizi nitazitowesha mikononi pako, nao waaguaji hawatakuwako kwako. Tena ndipo, nitakapovitowesha kwako vinyago vyako na nguzo zako za mawe za kutambikia, usiangukie tena yaliyo kazi za mikono yako. Hata mifano yenu ya mwezi nitaing'oa kwako, nayo miji yako nitaiangamiza. Kwa makali yenye moto nitawalipisha wamizimu wasiosikia. Yasikieni, Bwana anayoyasema: Haya! Bisheni mbele ya milima, vilima vizisikie sauti zenu! Ninyi milima, yasikieni masuto ya Bwana! Yasikieni nanyi miamba mlio misingi ya nchi! Kwani Bwana ana shauri nao walio ukoo wake, hana budi kuumbuana na Waisiraeli! Ninyi mlio ukoo wangu, nimewafanyizia nini? Nimewachokoza kwa nini? Nijibuni! Kwani niliwatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta huku, nikawakomboa katika nyumba, mlimokuwa watumwa, nikamtuma Mose na Haroni na Miryamu, wawatangulie. Mlio ukoo wangu, yakumbukeni, Balaka, mfalme wa Moabu, aliyowawazia, nayo Bileamu, mwana wa Beori, aliyomjibu! Yakumbukeni nayo yaliyofanyika toka Sitimu mpaka Gilgali, mpate kujua, ya kuwa Bwana ni mwongofu. Nimtokee Bwana na kumpa nini nikimnyenyekea Mungu Alioko huko juu? nimtolee ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, kama ndama za mwaka mmoja Je? Bwana atapendezwa na maelfu ya madume ya kondoo? Au atapendezwa na maelfu kumi ya vijito vya mafuta? Au nimpe mwanangu wa kwanza, awe ng'ombe ya tambiko ya kuondolea mapotovu yangu? Je? Zao la tumbo langu liyalipe makosa ya roho yangu? Umeambiwa, wewe mtu, yaliyo mema, nayo Bwana anayoyatafuta kwako: Yafanye yapasayo ukipenda kuwahurumia wenzako, tena ukiendelea kushikamana na Mungu wako na kujinyenyekeza. Sauti ya Bwana inawaita waliomo mjini, - nako kulitazamia Jina lako ni ujuzi - inasema: Isikieni fimbo iwapigayo! Msikieni naye aliyeiagiza! Je? Nyumbani mwao wasiomcha Mungu yangalimo bado malimbiko yaliyopatwa kwa uovu? nazo zile pishi nyembamba zilizoapizwa? Niwawazie kuwa wametakata, ijapo watumie mizani za kuchukulia mali za watu bure? au ijapo watie mishipini vijiwe vya kupimia vidanganyavyo watu? Matajiri ya kwao huzidi ukorofi, nao wenyeji wao husema uwongo, nazo ndimi zao vinywani mwao hudanganya watu. Kwa hiyo nami nitakupiga, usipone; nitakuangamiza kwa ajili ya makosa yako. Wewe utakula, lakini hutashiba, njaa ikae tumboni mwako. Utakayoyapeleka pengine hutayaponya; nayo utakayoyaponya, nitayatolea panga. Wewe utapanda, lakini hutavuna; wewe utakamua chekele, lakini hutajipaka mafuta; utakamua zabibu, lakini hutakunywa mvinyo. Kwani mmeyashika maongozi ya Omuri, mkayafanya matendo yote ya mlango wa Ahabu, mkayafuata mashauri yao, niigeuze nchi yenu, iwe mapori matupu, nao watakaokaa huku wazomelewe. Hivyo ndivyo, mtakavyotwikwa matusi yao walio ukoo wangu. Yamenipata! Kwani yamenijia mambo yapatikanayo penye mwisho wa machumo ya matunda, siku za kiangazi zikitimia, au watu wakiokotezaokoteza zabibu: hakuna kichala cha zabibu za kula wala kuyu tu, roho yangu inazozitunukia sana. Wamchao Mungu wametoweka katika nchi hii, kwa watu wa huku hakuna mwenye moyo unyokao. Wote huvizia, wamwage damu za watu, kila mmoja humtegea mwenziwe tanzi. Kama ni kufanya mabaya, mikono yote miwili iko tayari, yamalizike vema. Mkuu ayatakayo, mwenye kukata mashauri huyafanya akipenyezewa mali; mwenye nguvu akiyasema, roho yake inayoyatamani, basi, yayo hayo wanayafunganyafunganya. Aliye mwema kwao hufanana na mbigili, anyokaye moyo kwao ni mbaya kuliko boma la migunga. Siku, wapelelezi wako waliyoisema, ile siku, utakapopatilizwa, inakuja! Ndipo, watakapochafukwa na mioyo. Usimtegemee mwenzio! Wala usimjetee rafiki yako umpendaye! Ilinde midomo ya kinywa chako, mwanamke alalaye kifuani pako asiyajue yaliyomo! Kwani mwana wa kiume anambeza baba yake, naye mwana wa kike anamwinukia mama yake, vilevile mkwe na mkwewe, nao watakaomchukiza mtu ndio waliomo mwake. Lakini mimi nitamchungulia Bwana, nimngojee Mungu wangu atakayeniokoa. Mungu wangu atanisikia. Usinifurahie, uliye adui yangu! Kama ningeanguka, nitainuka tena. Kama ninakaa gizani, Bwana ni mwanga wangu. Makali yake Bwana nitayavumilia, kwani nimemkosea: mwisho atanigombea magomvi yangu, anikatie shauri lililo sawa, atanitoa na kuniweka mwangani, nipate kuuona wongofu wake. Naye adui yangu ataviona; ndipo, soni itakapomfunika, yeye aniulizaye sasa: Bwana Mungu wako yuko wapi? Macho yangu yatamfurahia, atakapokanyagwa kama taka ya barabarani. Siku itakuja, kuta zako zitakapojengwa, siku hiyo mipaka yako itakuwa mbali. Siku hiyo watakuja kwako watokao Asuri na miji ya Misri, tena kutoka Misri mpaka mto huo mkubwa, tena kutoka bahari hii mpaka bahari ya pili, tena kutoka mlima huu mpaka mlima ule. Lakini kwanza nchi hii sharti iwe mapori tu kwa ajili yao waikaao; hayo ndiyo mapato ya matendo yao. Walio ukoo wako wachunge kwa fimbo yako, ndilo kundi lililo fungu lako. ni wao wakaao peke yao katika mwitu huko Karmeli, walishe hata Basani na Gileadi kama siku za kale. Kama siku zile, mlipotoka katika nchi ya Misri, nitawaonyesha mambo yatakayowastaajabisha. Wamizimu watakapoyaona, watapatwa na soni, nguvu zao zote zikiwa za bure, wataweka mikono vinywani, nayo masikio watayaziba, yasisikie. Watalamba mavumbi kama nyoka, kama wadudu watambaao chini watatoka mafichoni mwao na kutetemeka, wamjie Bwana Mungu wetu kwa kutishika, nawe wewe watakuogopa. Je? Yuko Mungu afananaye na wewe, aondoaye maovu, ayapitaye mapotovu yao walio masao yao waliokuwa fungu lake? Hazishiki kale na kale nguvu za makali yake, kwani hupendezwa na kuwaendea watu kwa upole. Nasi atatuhurumia tena, maovu yetu yote atayapondaponda, yatutoke, makosa yetu yote atayatupa vilindini mwa bahari. Yakobo utamwendea kwa welekevu, naye Aburahamu kwa upole, kama ulivyowaapia baba zetu tangu siku zile za kale. Hili ndilo tamko zito la kuuambia Niniwe yatakayoupata, ni kitabu cha maono, Nahumu wa Elkosi aliyoyaona. Bwana ni Mungu mwenye wivu alipizaye; kwani Bwana ni mlipizaji mwenye makali, Bwana huwalipiza wapingani wake, nao wachukivu wake huwashikia makali. Bwana ni mvumilivu, mwenye nguvu kuu, lakini aliye mkosaji hamwachilii, asimpatilize. Njia yake Bwana imo katika kimbunga na katika upepo mkali, nayo mawingu ndiyo mavumbi ya miguu yake. Akiikaripia bahari, anaipwelesha, nayo mito mikubwa yote anaikausha. Nchi za Basani na za Karmeli zimezimia, nayo majani na maua ya Libanoni yamezimia. Milima hutetemeka mbele yake, navyo vilima hutikisika; nayo nchi huinukia usoni pake pamoja na ulimwengu nao wote wakaamo. Yuko nani awezaye kusimama, akimkasirikia? Au yuko nani awezaye kukaa katika makali yake yenye moto? Hasira yake ichomayo humwagika kama moto wenyewe, nayo miamba hupasuliwa nayo. Bwana ni mwema, ni ngome siku ya masongano, huwajua wamkimbiliao. Lakini kwa mafuriko ya maji yatosayo atapamaliza mahali pao wengine, nao wachukivu wake atawakimbiza gizani. Mwawaziaje kumpingia Bwana? Yeye ndiye atakayewamaliza, masongano yasitokee mara ya pili. Ingawa washikamane kama miiba iliyosukwa, au ingawa waloe kwa mvinyo, wawe majimaji kama mvinyo zao, wote pia wataliwa na moto kama majani makavu. Mwako wewe ametoka awazaye mabaya ya kumpinga Bwana kwa mashauri maovu, aliyoyatoa. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ingawa wakae na kutulia kwa kuwa wengi hivyo, watakatwa, watoweke. Lakini wewe, kama nimekunyenyekeza, sitakunyenyekeza tena. Sasa nitayavunja makongwa yao, yakuondokee, nayo mafungo uliyofungwa nitayararua. Lakini kwa ajili yako (Asuri) Bwana ameagiza, wenye jina lako wasipewe tena kuzaa, namo nyumbani mwa mungu wako nitavitowesha vinyago vya kuchonga navyo vya kuyeyusha, nawe nitakuchimbia kaburi lako, kwani umeonekana kuwa mwepesi zaidi. Tazameni! Milimani juu iko miguu ya mpiga mbiu atangazaye utengemano: Uzile sikukuu zako, Yuda! Vilipe viapo vyako! Kwani yule mwovu asiyefaa hatapita tena kwako, amekwisha kung'olewa wote pia. Amepanda mwenye kutawanya, akujie; kwa hiyo lilinde boma na kuiangalia njia! Jifunge sana viuno vyako! Nazo nguvu, ulizo nazo, zikaze kabisa! Kwani Bwana anaurudisha utukufu wake Yakobo nao utukufu wake Isiraeli, kwani wapokonyi waliyapokonya yaliyokuwako, nayo matawi ya mizabibu yao waliyaharibu. Ngao za mafundi wake wa vita ni nyekundu, watu wake wenye nguvu wanavaa nguo nyekundu za kifalme, siku, yanapopangwa, vyuma vya magari yake humetuka kama moto, nayo mikuki yake hutikiswatikiswa. Barabarani magari yanapiga vishindo vya nguvu, namo uwanjani yanashindana mbio; mkiyatazama huwa kama mienge ya moto, tena hurukaruka upesi kama umeme. Basi, anawakumbuka wakuu wake, lakini wanakuja na kujikwaakwaa; walipokwenda mbiombio kuufikia ukuta wa boma la nje, kikingio cha kuubomolea kilikuwa kimekwisha kuwekwa. Malango ya upande wa mtoni yalipofunguliwa, waliomo jumbani mwa mfalme wakayeyuka. Mke wa mfalme hana budi kuvuliwa nguo na kupelekwa mbali, vijakazi wake wakilia kama sauti za hua na kujipigapiga vifua. Niniwe ulikuwa kama ziwa la maji tangu kale, lakini sasa hao wengi wanajikimbilia tu; wanaambiwa: Simameni! Simameni! Lakini hakuna anayegeuka. Tekeni fedha! Tekeni dhahabu! Kwani malimbiko hayana mwisho; viko vyombo vya kila namna vipendezavyo. Lakini kwa kuwa mioyo imeyeyuka, uko uchi na utupu na ukiwa, nayo magoti yanagotanagotana, viuno vyote vinatetemeka, nazo nyuso zao wote zimewapoa. Makao ya simba yako wapi? Malisho ya wana wa simba yako wapi nayo? Ndipo wapi, walipotembea simba mume na mke na watoto pasipo kuona awastushaye? Ndipo wapi, simba waliporarua nyama, mpaka watoto wao washibe? Ndipo wapi, walipoona nyama wa kuwapatia nao wake zao? Ndipo wapi, walipojaza mapango yao nyama, waliowararua? Yako wapi mashimo yao nyama wao hao, waliowararua? Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Utaniona, nikikujia, niyachome magari yako, yawe moshi, nao wana wako wa simba upanga utawala; nitakukomesha, usirarue tena nyama katika nchi, wala sauti za wajumbe wako zisisikilike tena. Yataupata huo mji wenye damu! Wote mzima umejaa uwongo na ukorofi! Haukuacha kupokonya. Na wasikie uvumi wa mijeledi na vishindo vya magurudumu yatutumuayo na vya farasi wapigao mbio na vya magari yarukayo! Wapandao farasi watakuja mbiombio wenye panga ziwakazo moto na wenye mikuki imerimetayo kama umeme. Ndipo, watakapouawa wengi, mizoga iwe chungu zima, watu wakwazwe na mizoga. Hayo ndiyo malipo ya uzinzi mwingi wa huyo mzinzi mke aliye mzuri wa kupendeza, aliyenasa kwa uganga wake, aliyeteka makabila mazima kwa uzinzi wake na milango ya watu kwa uganga wake. Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Utaniona, nikikujia, nizifunue nguo zako ndefu nikizipandisha mpaka usoni kwako, nionyeshe mataifa uchi wako, nao walio wa kifalme niwaonyeshe yako yenye soni. Nitakutupia yatapishayo, nikutie soni; nitakuweka kuwa kitisho chao watakaokutazama. Ndipo, kila atakayekuona atapokukimbia na kusema: Kumbe Niniwe umebomolewa! Yuko nani atakayeombolezea? Nitatafuta wapi watakaokutuliza moyo? Je? U mwema kuliko No wa Amoni uliokaa majitoni huko Misri, uliozungukwa na maji? Boma lake ulikuwa wingi wa maji, nao ukuta wa nje wa boma ulikuwa wingi wa maji. Ulipata nguvu kule kwa Wanubi nako kwa Wamisri wasiohesabika, Waputi na Walubi walikuwa tayari kuusaidia. Nao umetekwa na kuhamishwa utumwani, nao watoto wake wachanga wakapondwa vichwa po pote pembeni barabarani; waliokuwa wenye utukufu wakapigiwa kura, nao wakuu wake wote wakafungwa minyororo. Wewe nawe na uleweshwe, uwe kama mtu azimiaye roho, wewe nawe na ujitafutie ngome ya kukimbilia adui. Maboma yako yote inafanana na mikuyu yenye kuyu za kwanza, mtu akiitikisa, zitaangukia kinywani mwake anayetaka kuzila. Waume wako, ulio nao mwako, utawaona kuwa kama wanawake, nayo malango ya nchi yako yatakuwa yamefunguka, yawe wazi mbele ya adui zako, nao moto utayala makomeo yako. Jichotee maji kuwa nayo siku za kusongwa, kayatengeneze maboma yako, yapate nguvu! Ukiisha kuuponda mchanga, ukanyage udongo, nayo tanuru ya kuchomea matofali itengeneze, ipate nguvu! Lakini patakapotimia, moto utakula, nazo panga zitakuangamiza zikikula kama funutu, ingawa mwe wengi kama funutu, ingawa mwe wengi kama nzige. Wachuuzi wako walikuwa wengi kuliko nyota za mbinguni, wakawa kama funutu: wakigeuka kuwa nzige, huruka kwenda zao. Wakuu wako wa serikali wanafanana na nzige, nao wakuu wako wa askari wanafanana na makundi ya nyenze: siku za baridi huja kulala kutani, lakini jua likitoka, hujiendea kwa kuruka, tena mahali, walipokwenda, hapajulikani. Wachungaji wako, mfalme wa Asuri, wamelala, watukufu wako wamelala usingizi. Watu wako wametawanyika milimani juu, tena hakuna anayewakusanya. Donda lako haliwezekani, pigo lililokupiga haliponi kabisa. Wote wazisikiao habari zako watakupigia makofi, kwani yuko nani, ambaye ubaya wako haukumpata siku zote? Bwana, hata lini nikulilie, unisaidie? Nawe husikii! Hata lini nikulalamikie kwa kukorofishwa? Nawe huniokoi! Mbona umeniacha, nione maovu, ukatazama tu, ninavyosumbuliwa? Uangamizo na ukorofi uko mbele yangu, yako magombano, hata mashindano hutokea. Kwa hiyo Maonyo yanakosa nguvu, mashauri yapasayo hayatokei kale na kale, kwani asiyemcha Mungu humnasa aliye mwongofu, kwa hiyo yanyokayo yakitokea yamekwisha kupotolewa. Yatazameni mambo yaliyoko kwa wamizimu, myaangalie! Ndipo, mtakapozizimka kwa kustuka. Kwani mimi hizi siku zenu nitatenda tendo, kama lingesimuliwa, msingeliitikia. Kwani mtaniona, nikiwainua Wakasidi, lile taifa kali lenye mioyo miepesi, ni wale wanaokwenda katika nchi za mbali, wajipatie makao yasiyo yao. Ndio watu watishao kwa kutia woga, kwao hao hutoka amri zilizo za majivuno tu. Farasi wao hupiga mbio kushinda machui, ni wepesi sana kuliko mbwa wa mwitu wawindao jioni. Wapanda farasi wa kwao hujitata; tena hao wapanda farasi wakija kutoka mbali huruka kama tai wakimbiliao kula. Wao wote hujia kukorofisha, nyuso zao zote pia zikiwa zimeelekea mbele, hukusanya mateka kama ni mchanga. Hao ndio watakaowafyoza wafalme, hata wakuu watawacheka; hao ndio watakaoteka kila boma, maana hulikusanyia mchanga kuwa boma, kisha huliteka. Baadaye hujiendea kama upepo, huenda zao na kuzidi kukosa, nguvu zao huziwazia kuwa mungu wao. Kumbe wewe Bwana, siwe Mungu wangu mtakatifu toka kale? Kwa hiyo hatutakufa. Wewe Bwana, umemweka, atupatilize; wewe Mwamba wetu, umemtia nguvu, atuchapue. Macho yako yanatakata, hayawezi kuyaona tu hayo mabaya, huwezi kabisa kuvitazama tu, watu wanavyosumbuliwa. Mbona sasa unawatazama tu wapokonyaji na kujinyamazia kimya, asiyekucha akimmeza aliye mwongofu kuliko yeye? Unataka, watu wawe kama samaki wa baharini au kama wadudu wakosao awatawalaye? Yeye amewapandisha hawa wote kwa ndoana, akawakamata namo katika nyavu zake, akawakusanya katika majarifa yake, kwa hiyo akafurahi na kupiga vigelegele. Kwa sababu hii huzitambikia nyavu zake, huyavukizia nayo majuya yake, kwani kwa msaada wao mafungu yake ni yenye manono, navyo vyakula vyake ni vyenye mafuta. Je? Kwa hiyo utamwacha, awatoe vivyo hivyo, wavu wake uliowakamata, akiendelea kuua mataifa mazima pasipo kuwahurumia? Na nije kusimama pangu pa kulindia, ningoje zamu mnarani juu! Na nichungulie, nione, atakayoniambia, niyajue, nitakayoyajibu kwa ajili ya malalamiko yangu. Bwana akaniitikia, akaniambia: Liandike, uliloliona, ulichore katika vibao, watu wapate kulisoma mumo humo upesi. Kwani hilo ono liko na siku zake, hazijatimia bado, lakini linajihimiza kumalizika, haliongopi. Ingawa likawie, lingojee! Kwani halina budi kuja, halitachelewa. Utaona, moyo wake umejitutumua wenyewe, haunyoki; lakini mwongofu atapata uzima kwa kumtegemea Mungu. Kweli mvinyo hudanganya: mtu mwenye majivuno hawezi kutulia, ingawa aupanue moyo wake kuwa kama kuzimu, ingawa awe kama kifo, hawezi kushiba, sharti akusanye kwake mataifa yote, kweli sharti ayapeleke kwake makabila yote ya watu. Je? Hao wote hawatamtungia mafumbo ya kumsimanga na kumfyoza kwamba: Yatampata achukuaye mengi yasiyo yake! Ataviweza mpaka lini? Hata mizigo mizima ya mali, wengine walizompa, awawekee, amejipa, ziwe zake. Je? Hawatainuka kwa mara moja, wakuumize? Hawataamka, wakusumbue? Ndipo, utakapotekwa nao! Kwa kuwa wewe ulipokonya mali za mataifa mengi, kwa hiyo wao wa masao ya makabila yote watazipokonya mali zako, wazilipize damu ya watu, ulizozimwaga, wakulipishe nayo makorofi, ambayo uliitendea nchi na miji na wenyeji wao wote. Yatampata aupatiaye mlango wake mapato mabaya, apate kujitengenezea kiota juu kwamba: ajiepushe mikononi mwao wabaya. Mashauri yako yatautia mlango wako soni: ulipoangamiza makabila mengi, umeikosesha roho yako. Kwani majiwe yaliyomo ukutani yatapiga kelele, nayo miti ya kipaga itaitikia. Yatampata ajengaye miji kwa damu na kuishupaza mitaa yake kwa mapotovu! Je? Hamjayaona yatokayo kwake Bwana Mwenye vikosi? Namwone: Makabila ya watu waliyoyasumbukia, huliwa na moto, nayo, mataifa waliyoyafanyia kazi na kujichokesha, huwa ya bure. Kwani nchi hii itajazwa nao waujuao utukufu wa Bwana, kama maji yanavyofurikia baharini na kuyafunika yote Yatampata amnyweshaye mwenziwe kinywaji, alichokichanganya na makali yake! Kisha anamlewesha, kusudi auone uchi wake na kumfurahia! Umejishibisha yatiayo soni ukiyaacha yenye utukufu, lakini wewe nawe sharti unywe, ujulikane kuwa mtu asiyetahiriwa. Kikombe kilichomo kuumeni mwa Bwana kinakufikia, utukufu wako ufunikwe nayo yenye soni. Kwani makorofi, ambayo uliitendea Libanoni, yatakufunika, nao nyama, uliowaua bure tu, watakutia woga, kwa ajili ya damu za watu, ulizozimwaga kwa kuikorofisha nchi na miji pamoja na wenyeji wao wote. Hapo kinyago kilichochongwa kitafaaje? Maana ni kazi tu ya fundi aliyekichonga. Au kinyago cha vyuma vilivyoyeyushwa kifundishacho uwongo tu kitafaaje? Maana ni egemeo lake fundi aliyekitengeneza, apate miungu isiyosema. Yatampata akiambiaye kipande cha mti: Amka! naye akiambiaye kipande cha jiwe lisilosema: Inuka! Je? Hicho kitaweza kufumbua neno? Kitazame! Kimefunikwa na dhahabu na fedha, lakini ndani yake hamna pumzi yo yote. Lakini Bwana yumo Jumbani mwake mwenye utakatifu, usoni pake kila mtu wa nchi hii anyamaze kimya! Bwana, nimeusikia utume wako, nikaogopa. Bwana, itokeze kazi yako, iwepo katika miaka ijayo! Ijulishe katika miaka ijayo! Ukikasirika zikumbuke huruma! (Kituo.) Mungu alikuja toka Temani, Mtakatifu alitoka mlimani kwa Parani. Utukufu wake huzifunika mbingu, nchi hii nayo hujaa matukuzo yake. Huangaza kama mwanga wa jua, miali hutoka mkononi mwake; ndimo, nguvu zake zifichikamo. Magonjwa yauayo humtangulia, nazo homa kali huifuata miguu yake. Anaposimama ndipo, anapoitetemesha nchi; anapochungulia ndipo, anapoyastusha mataifa. Milima iliyoko toka kale huatuka, vilima vilivyoko kale na kale huangukiana chini; ni vilevile, alivyovikanyaga juu tangu kale alipopita. Vijumba vya Wanubi niliviona vyenye shida, nayo mahema ya nchi ya Midiani yakatikisika. Je? Bwana anaikasirikia mito? Makali yako yataitokea mito? Je? Machafuko yako yanaiendea bahari? Kwa kuwa unavutwa na farasi katika gari lako lishindalo! Uta wako umefunuliwa, utokee waziwazi, kama ulivyoziapia koo za watu kwa neno lako (Kituo.) Unapoipasua nchi, hapo hutokea majito. Ukioneka, milima hustuka, nayo mafuriko ya maji huzidi, vilindi vya baharini huvuma na kuikweza mikono yao juu. Jua na mwezi husimama kwao, mishale yako ikija kumulika, nao umeme wa mkuki wako ukimetameta. Kwa kukasirika unaikanyaga nchi, kwa kuchafuka unayaponda mataifa. Umetokea kuwaokoa walio ukoo wako, upate kumwokoa uliyempaka mafuta, ukaviponda vichwa vyao wasiokucha nyumbani mwao, ukazibomoa toka misingi hata vipaani. (kituo.) Kwa mikuki yao unavichoma vichwa vya vikosi vyao vijavyo mbio kama kimbunga kunikimbiza mimi na kunizomea kama watu wanaotaka kula mnyonge fichoni pake. Lakini wewe ukaja na kuikanyaga bahari ukipanda farasi wako, ijapo maji mengi yavume. Nilipoyasikia, ndipo, tumbo langu lilipotetemeka, midomo yangu nayo ikajipigapiga kwa uvumi wao, ugonjwa wa ubovu ukaingia mifupani mwangu, nikatetemeka wote hata chini, niliposimama, kwa sababu sina budi kuingoja siku ya kusongwa, itakapolipata lile kabila lililokuja kutushambulia. Kwani mkuyu hauchanui, wala mizabibu haizai, vichipukizi vya mchekele navyo hudanganya, mashamba ya ngano hayaleti chakula, kondoo wametoweka mazizini kwao, hata ng'ombe hamna vibandani mwao. Lakini mimi ninayemfurahia, ndiye Bwana, ninamshangilia Mungu wangu aliyeniokoa. Bwana Mungu ndiye aliye nguvu yangu! Anipa miguu ipigayo mbio kama yake kulungu, akiniendesha vema, nifike juu vilimani kwangu. Kwa mwimbishaji, ayaimbie mazeze yangu. Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Sefania, mwana wa Kusi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hizikia, siku zile, Yosia, mwana wa Amoni, alipokuwa mfalme wa Yuda. Ndivyo, asemavyo Bwana: Nitayakusanya kabisa yote pia na kuyaondoa juu ya nchi: nitawakusanya na kuwaondoa watu na nyama, nao ndege wa angani, nao samaki wa baharini nitawakusanya na kuwaondoa, nayo makwazo pamoja nao wasiomcha Mungu, niwatoweshe watu juu ya nchi hii. Ndivyo, asemavyo Bwana: Nitaukunjua mkono wangu, uwakamate Wayuda nao wote wakaao Yerusalemu; masao yote ya Baali nitayatowesha mahali hapa, majina yao watangazaji pamoja nayo ya watambikaji. Nao wanaokitambikia kikosi cha mbinguni juu ya paa pamoja nao wanaomtambikia Bwana juujuu, kwani huapa na kumtaja Yeye, tena huapa na kumtaja mfalme wao. Nao waliorudi nyuma na kumwacha Bwana, hawamtafuti Bwana, wala hawamchungulii. Nyamazeni kimya usoni pa Bwana Mungu! Kwani siku ya Bwana iko karibu, kwani Bwana amekwisha kulilinganya tambiko, akawaeua walioalikwa naye. Itakuwa siku ya tambiko la Bwana, ndipo, nitakapowapatiliza wakuu nao wana wa mfalme, nao wote waliojivika mavazi mageni. Siku hiyo ndipo, nitakapowapatiliza wote warukao juu ya kizingiti, nao wanaoijaza Nyumba ya Bwana, wao wakorofi na wadanganyifu. Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku hiyo itakuwa, makelele yasikilike penye Lango la Samaki, na vilio katika mitaa ya nje na uvumi wa maanguko makuu vilimani. lieni, mkaao penye barabara ya Vinu! Kwani kabila zima la wachuuzi litakuwa limeangamizwa, watatoweshwa wote wachukuao fedha! Siku hizo itakuwa, nitakapochunguzia Yerusalemu kwa mienge ya moto, niwavumbue wajikaliao tu penye shimbi za mvinyo zao na kusema mioyoni mwao: Bwana hafanyi wala mema wala mabaya. Mali zao zote zitakuwa mateka, nazo nyumba zao zitakuwa mahame; watajenga nyumba, lakini hawatakunywa mvinyo zao. Siku ya Bwana iliyo kuu iko karibu, iko karibu kweli, inataka kutimia upesi. Uvumi wa siku ya Bwana utakaposikilika, ndipo, naye mnguvu atakapolia kwa uchungu. Siku hiyo ni siku ya machafuko, ni siku ya kusongeka na ya kubanwa, ni siku ya uangamivu na ya upotevu, ni siku yenye giza na weusi, ni siku yenye mawingu meusi kama ya usiku, ni siku ya kupiga mabaragumu na yowe ya kutisha miji yenye maboma na minara mirefu. Ndipo, nitakapowaogopesha watu, wajiendee kama vipofu, kwani wamemkosea Bwana! Nazo damu zao zitamwagwa kama mavumbi, nazo nyama za miili yao zitatupwa kama mavi. Hata fedha zao na dhahabu zao hazitaweza kuwaponya siku hiyo ya machafuko ya Bwana; katika moto wa wivu wake nchi hii yote nzima itateketea, kwani wote wakaao katika nchi hii atawaishiliza wote pia, wakiguiwa na kituko kwa mara moja. Jikusanyeni, jikusanyeni, mlio taifa lisilokata tamaa, shauri likiwa halijafanyika bado! Kwani siku hiyo inakuja mbio kama makapi yapeperushwayo. Kwa kuwa makali ya Bwana yenye moto hayajawafikia bado, kwa kuwa siku ya makali ya Bwana haijawafikia bado, mtafuteni Bwana, ninyi wanyenyekevu wote wa nchi hii mnaoyafanya yanyokayo mbele yake! Utafuteni wongofu! Utafuteni unyenyekevu nao! Kwa njia hii labda mtaona pa kujifichia, siku ya makali ya Bwana itakapotimia. Kwani Gaza utakuwa umeachwa, nao Askaloni utakuwa mapori matupu, Waasdodi watakimbizwa mchana, nao Ekroni utabomolewa. Yatawapata nanyi mkaao pwani, mlio wa taifa la Wakreta! Neno la Bwana litatimia kwenu wa Kanaani, nako kwenu wa nchi ya Wafilisti kwamba: Nitakuangamiza, pasisalie mwenyeji. Ndipo, nchi ya pwani itakapokuwa nyika yenye visima na mazizi ya kondoo, watakaowachunga huko. Nchi hii itakuwa yao wakaosalia wa mlango wa Yuda; wao ndio watakaochunga huko, tena jioni watakwenda kulala katika nyumba za Askaloni; kwani Bwana Mungu wao atawakagua, ayafungue tena mafungo yao. Nimeyasikia matusi ya Wamoabu nao ufyozaji wa wana wa Amoni, wakiwatukana walio ukoo wangu na kujivuna kwa kuingia katika mipaka yao. Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli: Kweli kwa hivyo, nilivyo Mwenye uzima, nchi ya Moabu itakuwa kama Sodomu nayo nchi ya wana wa Amoni kama Gomora, zitageuka kuwa kwenye viwawi, zitakuwa mashimo ya chumvi na mapori matupu kale na kale. Masao yao walio ukoo wangu watawanyang'anya mali zao, watakaosalia wa taifa langu watawachukua, wawe watumwa wao. Hayo yatawapata kwa ajili ya majivuno yao, kwani wamejikuza na kuwatukana walio ukoo wa Bwana Mwenye vikosi na kuwazomea. Bwana ataogopwa kwao, kwani miungu yote ya hapa nchini ataitowesha, wamwangukie wote, kila mtu mahali pake, hata visiwa vyote vya wamizimu. Nanyi Wanubi, mtapigwa na upanga wangu, mfe. Kisha ataukunjua mkono wake na kuuelekeza kaskazini, awaangamize Waasuri, nao Niniwe ataugeuza kuwa mapori matupu na nchi kavu kama nyika. Mwake yatalala makundi mazima ya kila nyama wa nchi za mataifa, hata korwa na nungu watalala katika vichwa vya nguzo zake, sauti za bundi zitasikilika madirishani, penye vizingiti patajaa takataka, kwani mbao za miangati zitakuwa zimeondolewa. Hayo ndiyo yatakayoupata huo mji uliojaa furaha uliokaa pasipo kuhangaika kabisa, uliosema moyoni mwake: Mji ni mimi, hakuna mwingine tena! Kumbe umegeuka kuwa mapori matupu na makao ya nyama wa porini! Kila atakayepapita atauzomea na kuupungia kwa mkono wake. Yataupata huo mji usiotii, uliojichafua kwa makorofi yake! Haukusikia ulipoambiwa neno, ukakataa kuonyeka, haukumtegemea Bwana, ukakataa kumkaribia Mungu wake. Wakuu wake waliomo mwake ni simba wangurumao, waamuzi wake ni mbwa wa mwitu wakila jioni hawaweki ya asubuhi. Wafumbuaji wake hujikuza kwa maneno, ni watu wasiotegemeka; watambikaji wake hupachafua Patakatifu, tena huyapotoa Maonyo. Lakini Bwana ni mwongofu, yuko katikati yao, hafanyi upotovu; kila kunapokucha hutokeza mwangani mashauri yake yaliyo sawa, lakini mpotovu hataki kuyajua yamtiayo soni. Nimetowesha mataifa, maboma yao yenye minara yako peke yao tu; nazo barabara za kwao nimezigeuza kuwa za bure, kwani hakuna mtu tena apitaye hapo, miji yao imebomolewa, hakuna watu wakaao humo hata mmoja. Nalisema: Sasa utaniogopa, uonyeke, makao yasitoweshwe, yasitimizwe yote, niliyoyataka kuwapatilizia; lakini wao walijihimiza sana kufanya maovu katika matendo yao yote. Ndivyo, asemavyo Bwana: Kwa hiyo ningojeni, hata siku ifike, nitakapoondokea kuteka mateka! Kwani shauri langu ni kukusanya mataifa na kuwapeleka mahali pamoja wenye nchi za kifalme, niwamwagie machafuko yangu na makali yangu yote yaliyo yenye moto, kwani ndipo, nchi hii yote nzima itakapoteketezwa kwa moto wa wivu wangu. Kwani hapo ndipo, nitakapoigeuza midomo ya makabila ya watu, iwe imetakata, wao wote pia walitambikie Jina la Bwana na kumtumikia kwa kuwa kundi moja. Toka ng'ambo ya pili ya mito ya Nubi watawaleta waninyenyekeao, wawe kipaji cha kunipa, ndio wana wangu waliotawanyika. Siku hiyo hutapatwa na soni kwa ajili ya matendo yako yote, uliyonikosea, kwani hapo ndipo, nitakapowaondoa katikati yako walioyafurahia majivuno yako, usiendelee tena kujikuza mlimani penye Patakatifu pangu. Nitasaza mwako watu walio wanyonge na wanyenyekevu watakaolijetea Jina la Bwana. Masao ya Isiraeli hawatafanya upotovu, wala hawatasema uwongo, wala vinywani mwao hamtaonekana ndimi zenye udanganyifu, kwani wao watajilisha wenyewe, kisha watalala na kupumzika, pasipo kuona atakayewastusha. Piga vigelegele, binti Sioni! Shangilieni, ninyi Waisiraeli! Nawe binti Yerusalemu, furahiwa kwa moyo wote! Bwana ameyatangua mashauri, uliyokatiwa, akamwondoa adui yako! Mfalme wa Isiraeli ni Bwana alioko katikati yako, hutaogopa mabaya tena. Siku hiyo Yerusalemu utaambiwa: Usiogope! Nawe Sioni utaambiwa: Mikono yako isilegee tena! Bwana Mungu wako yuko katikati yako, naye ni Mungu ajuaye kuokoa. Atakufurahia na kukufurahisha, atatulia kwa kukupenda, atakushangilia na kukuimbia. Wenye masikitiko wasioingia mikutano ya sikukuu nitawakusanya, kwani nao ni wa kwako, ingawa wawe wametwikwa yawatiayo soni. Mtaniona, siku hizo nikiwapatia mambo wote wanaokutesa, niwaokoe wachechemeao, niwakusanye nao waliofukuzwa, watukuzwe, nikiwapatia jina kuu katika hizo nchi zote, walikotiwa soni. Siku hizo ndipo, nitakapowapeleka kwenu ni siku hizo, nitakapokwisha kuwakusanya, kwani nitawapatia ninyi jina kuu, mtukuzwe kwa makabila yote ya nchi hii, nitakapoyafungua mafungo yenu machoni pao. Bwana ndiye anayeyasema! Katika mwaka wa pili wa mfalme Dario katika mwezi wa sita siku ya kwanza ya mwezi kwa msaada wa mfumbuaji Hagai neno la Bwana lilimjia Zerubabeli, mwana wa Saltieli, aliyekuwa mtawala nchi ya Yuda, na mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema kwamba: Wao wa ukoo huu husema: Siku ya kujengwa kwake Nyumba ya Bwana, siku hizo hazijaja bado. Kwa hiyo neno la Bwana lilikuja kwa msaada wa mfumbuaji Hagai la kwamba: Je? Siku hizi inawapasa ninyi kukaa katika nyumba zilizopambwa kwa mbao, Nyumba hii ikikaa kuwa kama hame? Hivi ndivyo, Bwana mwenye vikosi anavyosema sasa: Ielekezeni mioyo yenu, izitazame njia zenu! Mmepanda mengi, mkavuna machache; mnapokula hamshibi, mnapokunywa, kiu haiishi; mnapovaa, baridi haiondoki miilini; afanyaye kazi ya mshahara huutia mshahara katika mfuko wenye matundu. Hivi ndivyo, Bwana mwenye vikosi anavyosema: Ielekezeni mioyo yenu, izitazame njia zenu! Pandeni milimani, kaleteni miti, mwijenge hiyo Nyumba! Ndipo, nitakapopendezwa nayo, nitokeze humo utukufu wangu; ndivyo, Bwana anavyosema. Mliwaza kupata mengi, lakini mlipoyatazama, yalikuwa machache, nayo mliyoyapeleka nyumbani, nikayapeperusha; hivyo ni kwa sababu gani? ndivyo, aulizavyo Bwana Mwenye vikosi. Ni kwa ajili ya Nyumba yangu iliyo hame tu, nanyi mnajihimiza kila mtu kuijenga nyumba yake. Kwa sababu hii mbingu zimewanyima umande, nayo nchi ikawanyima mazao. Nikauita ukavu, uzijie nchi na milima hii na ngano na pombe mbichi na mafuta nayo yote pia, nchi iyazaayo, uwajie nao watu na nyama na mapato yote ya mikono. Ndipo, Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, nayo masao yote ya huo ukoo walipoisikia sauti ya Bwana Mungu wao nayo maneno ya mfumbuaji Hagai, Bwana Mungu aliyemtuma kuwaambia hayo, nao wa ukoo huu wakamwogopa Bwana. Ndipo, Hagai aliyetumwa na Bwana alipowaambia wao wa ukoo huu kwa kuagiziwa huo utume na Bwana, akasema: Ndivyo, asemavyo Bwana: Mimi niko pamoja nanyi. Kisha Bwana akaiamsha roho ya mtawala nchi ya Yuda Zerubabeli, mwana wa Saltieli, nayo roho ya mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, nazo roho zao masao yote ya ukoo huu, wakaenda kufanya kazi ya kuijenga Nyumba ya Bwana Mwenye vikosi aliyekuwa Mungu wao. Ikawa siku ya ishirini na nne ya mwezi wa sita katika mwaka wa pili wa mfalme Dario. Siku ya ishirini na moja ya mwezi wa saba neno la Bwana likaja kwa msaada wa mfumbuaji Hagai la kwamba: Mwambie mtawala nchi ya Yuda Zerubabeli, mwana wa Saltieli, na mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, nao walio masao ya ukoo huu, useme: Kwenu ninyi mliosalia yuko nani aliyeiona Nyumba hii, ilivyokuwa yenye utukufu wake wa kwanza? Tena sasa mnaiona kuwaje? Machoni penu siyo kama si kitu? Ndivyo, asemavyo Bwana: Sasa Zerubabeli, jipe moyo! Nawe mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, jipe moyo! Nanyi nyote mlio ukoo wa nchi hii, jipeni mioyo! Ndivyo, asemavyo Bwana: Fanyeni kazi, kwani mimi niko pamoja nanyi! ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Lile Neno, nililoliagana nanyi, mlipotoka Misri, lingaliko; nayo Roho yangu inakaa bado katikati yenu; kwa hiyo msiogope! Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Bado kitambo kidogo ndipo, nitakapozitetemesha mbingu na nchi, hata bahari na pakavu, nao wamizimu wote nitawatetemesha. Ndipo, yatakapotokea yapendezayo wamizimu wote, ndipo, nitakapoijaza Nyumba hii utukufu. Bwana Mwenye vikosi ameyasema. Yangu ni fedha, yangu ni dhahabu; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Utukufu wa Nyumba hii ya nyuma utakua kuliko ule wa Nyumba ya kwanza; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema; kwani mahali hapa nitawapatia watu utengemano; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa katika mwaka wa pili wa Dario neno la Bwana likaja kwa msaada wa mfumbuaji Hagai la kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Waulize watambikaji maana ya Maonyo ukisema: Kama mtu anachukua nyama takatifu katika upindo wa vazi lake, kisha kwa huo upindo anagusa mkate au ugali au mvinyo au mafuta au chakula cho chote, je? Nacho kitakuwa kitakatifu? Watambikaji wakajibu, wakasema: Hapana. Hagai akauliza tena: Inakuwaje? Mtu aliyejipatia uchafu kwa kugusa mfu, akigusa kimoja chao vitu hivyo, kitakuwa kichafu? Watambikaji wakajibu, wakasema: Ndio, kitakuwa kichafu. Hagai akajibu, akasema: Ndivyo, asemavyo Bwana: Ndivyo walio ukoo huu walivyo, ndivyo hili taifa lilivyo machoni pangu, ndivyo nazo kazi zote za mikono yao zilivyo, ndivyo navyo vipaji vyote wanavyonitolea vilivyo, vyote ni vichafu. Sasa ielekezeni mioyo yenu, mwone yaliyowapata kuanzia siku ya leo na siku zote zilizopita, mlipokuwa hamjaweka jiwe kwa jiwe penye Jumba la Bwana. Hapo pote yalikuwa hivyo: mtu alipofika penye chungu ya miganda ya ngano yenye pishi ishirini, zikapatikana kumi tu, au alipofika penye kamulio kuchota ndoo hamsini, zikapatikana ishirini tu. Nilikuwa nimewapiga ninyi, nikayaunguza mashamba na kuyakausha kabisa, tena nikayanyeshea mvua ya mawe, kazi zote za mikono yenu zisifae, lakini ninyi hamkurudi kwangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Sasa ielekezeni mioyo yenu, mwone yatakayokuwa kuanzia siku hii ya leo na siku zote zitakazokuja tangu siku hii ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, ni kwamba tangu siku hii, msingi wa Jumba la Bwana ulipowekwa. Basi, ielekezeni mioyo mwone, kama mbegu za kupanda zitakaa tena chanjani, kama mizabibu na mikuyu na mikomamanga na michekele itaacha tena kuzaa; kuanzia siku hii ya leo nitakubariki. Neno la Bwana likamjia Hagai mara ya pili siku ya ishirini na nne ya mwezi huo la kwamba: Mwambie mtawala nchi ya Yuda Zerubabeli kwamba: Mimi nitazitetemesha mbingu na nchi; ndipo, nitakapovifudikiza viti vya kifalme vya wafalme, nazo nguvu za nchi za kifalme za wamizimu nitaziangamiza; tena nitayafudikiza magari nao walioyapanda, farasi waanguke pamoja nao waliowapanda, wauawe kila mmoja kwa upanga wa ndugu yake. Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Siku hiyo ndipo, nitakapokuchukua wewe Zerubabeli, mwana wa Saltieli, kwa kuwa u mtumishi wangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Nitakutunza kama pete yangu yenye muhuri, kwani nimekuchagua; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Katika mwezi wa nane katika mwaka wa pili wa Dario neno la Bwana lilimjia mfumbuaji Zakaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, kwamba: Bwana alikuwa amewakasirikia sana baba zenu. Kwa hiyo uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Rudini kwangu! ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi; ndipo, nami nitakaporudi kwenu; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Msiwe kama baba zenu walioambiwa na wafumbuaji wa kwanza kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Rudini na kuziacha njia zenu mbaya na kazi zenu mbaya! Lakini hawakusikia, wala hawakunitegea masikio; ndivyo, asemavyo Bwana. Basi, baba zenu wako wapi? Nao wafumbuaji watakuwapo kale na kale? Ila maneno yangu na maagizo yangu, niliyowaagiza watumishi wangu wafumbuaji kuyatangaza, hayakutimia kwa baba zenu? Ndipo, walipojirudia na kusema: Kama Bwana Mwenye vikosi alivyowaza moyoni kutufanyizia kwa ajili ya njia zetu na kwa ajili ya matendo yetu, ndivyo, alivyotufanyizia kweli. Siku ya ishirini na nne ya Mwezi wa kumi na moja, ndio mwezi wa Sebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la Bwana likamjia mfumbuaji Zakaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, kwamba: Usiku huu nimeona mambo: nimeona mtu aliyepanda farasi mwekundu; naye alikuwa amesimama katikati ya miti ya vihagilo iliyoko huko chini bondeni, nyuma yake walikuwa farasi wekundu na wa kijivujivu na weupe. Nikauliza: Wa nini hawa, Bwana wangu? Akaniambia yule malaika aliyesema na mimi: Mimi nitakuonyesha, kama hawa ni wa nini. Akajibu yule mtu aliyesimama katikati ya vihagilo, akasema: Hawa ndio, Bwana aliowatuma kutembea katika nchi po pote. Wakamjibu malaika wa Bwana aliyesimama katikati ya vihagilo, wakasema: Tumetembea po pote katika nchi, tukaiona nchi yote nzima, ya kuwa inatulia kimya. Ndipo, malaika wa Bwana alipojibu akisema: Bwana Mwenye vikosi, utaacha mpaka lini kuuhurumia Yerusalemu nayo miji ya Yuda, uliyoikasirikia hii miaka 70? Bwana akamjibu malaika aliyesema na mimi, akamwambia maneno mema ya kuutuliza moyo. Kisha malaika aliyesema na mimi akaniambia: Tangaza kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Nimeingiwa na wivu mwingi kwa ajili ya Yerusalemu na kwa ajili ya Sioni. Tena mimi ninawakasirikia sanasana wao wa hayo mataifa yanayokaa na kutulia; kwani nilipokasirika, ilikuwa kidogo tu, lakini wao wamejihimiza kuwafanyia mabaya. Kwa hiyo Bwana anasema hivi: Nimeugeukia Yerusalemu tena kwa huruma nyingi, Nyumba yangu ijengwe tena mwake; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi, hata kamba za kupimia viwanja zitavutwa tena mle Yerusalemu. Kisha tangaza kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Miji yangu itafurikiwa tena na mema yote, naye Bwana ataituliza tena mioyo ya Wasioni, maana atauchagua tena Yerusalemu, uwe wake. Nilipoyainua macho yangu, nichungulie, mara nikaona pembe nne. Nikamwuliza malaika aliyesema na mimi: Za nini hizi? Akaniambia: Hizi ndizo pembe zilizowatawanya Wayuda na Waisiraeli na Wayerusalemu. Kisha Bwana akanionyesha wafua vyuma wanne. Nikauliza: Hawa wanakuja kufanya nini? Akajibu kwamba: Hizo ndizo pembe zilizowatawanya Wayuda, asipatikane hata mtu mmoja aliyeweza kukiinua kichwa chake. Lakini hawa wamekuja kuzitisha na kuzibwaga zile pembe za wamizimu walioziinua pembe zao na kuzielekezea nchi ya Yuda, wapate kuwatawanya waliokuwako. Nilipoyainua macho yangu, nichungulie, mara nikaona mtu, naye alishika mkononi mwake kamba ya kupimia. Nikamwuliza: Unakwenda wapi? Akaniambia: Ninakwenda kuupima Yerusalemu, nione, upana wake na urefu wake ulivyo. Mara malaika aliyesema na mimi akatoka, kisha malaika mwingine akatokea kukutana naye, akamwambia: Piga mbio, umwambie yule kijana kwamba: Yerusalemu utakaa watu pasipo boma kwa wingi wa watu na nyama watakaokuwamo mwake. Kisha mimi nitakuwa boma la moto litakalouzunguka nao utukufu wake uliomo mwake utakuwa mimi; ndivyo, asemavyo Bwana. Ndivyo, asemavyo Bwana: Haya! Haya! Kimbieni, mwitoke nchi hiyo ya kaskazini! Kwani nimewatawanya ninyi katika pande zote nne za upepo wa angani; ndivyo, asemavyo Bwana. Haya! Jiponye, Sioni ukaaye kwake binti Babeli! Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kuutokeza utukufu amenituma kwa wamizimu walioziteka mali zenu ninyi, kwani anayewagusa ninyi huigusa mboni ya jicho lake. Ndipo, mtakaponiona, nikiwapungia kwa mkono wangu; ndipo, wao watakapokuwa mateka yao walio watumwa wao, mpate kujua, ya kuwa Bwana Mwenye vikosi amenituma. Shangilia kwa furaha, binti Sioni! Kwani utaniona, nikija kukaa katikati yako; ndivyo, asemavyo Bwana. Siku hiyo itakuwa, wamizimu wengi waje kuandamana na Bwana; ndipo, wao nao watakapokuwa ukoo wangu. Nitakaa katikati yako, upate kujua, ya kuwa Bwana Mwenye vikosi amenituma kwako. Ndipo, Bwana atakapowatwaa Wayuda, wawe fungu lake katika nchi hii takatifu, nao Yerusalemu atauchagua tena, uwe mji wake. Wote wenye miili ya kimtu sharti wanyamaze kimya usoni pake Bwana, kwani amekwisha kuondoka katika Kao lake takatifu! Kisha akanionyesha mtambikaji mkuu Yosua, akisimama mbele ya malaika wa Bwana, naye Satani alikuwa amesimama kuumeni kwake kumsengenya. Bwana akamwambia Satani: Bwana na akukemee wewe, Satani! Yeye Bwana aliyeuchagua Yerusalemu, uwe mji wake, na akukemee wewe! Kumbe huyu si kijinga kilichopona kwa kuokolewa motoni! Naye Yosua alikuwa amevaa nguo chafu aliposimama mbele ya malaika. Kisha huyu akasema na kuwaambia waliosimama mbele yake kwamba: Mvueni hizi nguo chafu! Akamwambia: Tazama, manza, ulizozikora, nimeziondoa kwako, nikakuvika nguo za sikukuu. Kisha akasema: Mfungeni kilemba kilichotakata kichwani pake! Wakamfunga kilemba kilichotakata kichwani pake pamoja na kumvika zile nguo, naye malaika wa Bwana alisimama papo hapo. Kisha malaika wa Bwana akamshuhudia Yosua kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kama utakwenda katika njia zangu na kuutumikia utumishi wangu, ndipo, wewe utakapoitunza Nyumba yangu na kuzilinda nyua zangu, kisha nitakupatia njia ya kufika kwangu katikati yao hawa wanaosimama hapa. Sasa sikia, wewe mtambikaji mkuu Yosua pamoja na wenzako wanaokaa mbele yako, kwani ndio watu wa kutazamiwa: Mtaniona, nikimleta mtumishi wangu Chipukizi. Kwani tazameni: Jiwe hili, nililoliweka mbele yake Yosua, macho saba yanalielekea jiwe hili moja; tena tazameni: Mimi ninachora humo machoro yanayolipasa, kisha nitaziondoa manza za nchi hii katika siku moja; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Siku hiyo ndipo, watakapoalikana mtu na mwenziwe kuja kukaa pamoja chini ya mzabibu na chini ya mkuyu. Kisha yule malaika aliyesema na mimi akarudi, akaniamsha kama mtu anayeamshwa katika usingizi wake. Akaniuliza: Unaona nini? Nikasema: Nimechungulia, nikaona kinara kilicho cha dhahabu tupu, nacho chombo chake cha mafuta kilikuwa juu yake, nazo taa zake zilikuwa saba, tena penye hizo taa zilizoko juu yake palikuwa na mirija saba ya kutilia mafuta. Kando yake iko michekele miwili, mmoja kuumeni penye chombo cha mafuta, mmoja kushotoni pake. Nikasema na kumwuliza malaika aliyesema na mimi kwamba: Vya nini hivi, Bwana wangu? Malaika aliyesema na mimi akajibu akiniambia: Je? Hujui, kama hivi ni vya nini? Nikasema: Sijui, Bwana wangu. Akajibu akiniambia kwamba: Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Zerubabeli la kwamba: Haitafanyika kwa vikosi wala kwa nguvu, ila kwa Roho yangu; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Nawe wewe mlima mkubwa ndiwe nani? Mbele ya Zerubabeli utageuka kuwa nchi tambarare, upate kulitoa jiwe la juu pembeni, wakimshangilia kwamba: Ppngezi! Pongezi! Ndipo, neno la Bwana liliponijia la kwamba: Mikono yake Zerubabeli imeweka msingi wa Nyumba hii, nayo mikono yake ndiyo itakayoimaliza. Ndipo, utakapojua, ya kuwa Bwana Mwenye vikosi amenituma kwenu. Kwani walioibeua siku ya mambo madogo ndio watakaofurahi wakiiona timazi mkononi mwa Zerubabeli; hizi taa saba ndio macho ya Bwana, ndiyo yanayotembea katika nchi hii nzima. Nikajibu na kumwuliza: Hii michekele miwili iliyoko kuumeni kwa kinara na kushotoni kwake ni ya nini? Nikaanza kusema mara ya pili na kumwuliza: Vichala hivi viwili vya michekele vilivyoko kando ya mirija ya dhahabu inayoyapeleka hayo mafuta yao ya dhahabu toka juu maana yao nini? Akaniambia kwamba: Je? Huijui maana yao? Nikasema: Siijui, Bwana wangu. Akaniambia: Hivi ndio wana wawili waliopakwa mafuta wanaosimama kwake Bwana wa nchi hii yote nzima. Nilipoyainua macho yangu tena, nichungulie, mara nikaona barua irukayo angani. Akaniuliza: Unaona nini? Nikasema: Mimi ninaona barua irukayo angani, urefu wake ni mikono ishirini, nao upana wake ni mikono kumi. Akaniambia: Hii ndio kiapizo kilichotika kuifikia nchi yote nzima, kwani kila mwizi ataondolewa huku, kama yalivyoandikwa upande wake mmoja, hata kila aapaye kiapo cha uwongo ataondolewa huku, kama yalivyoandikwa upande wake wa pili. Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Nimeitoa, ije kuingia nyumbani mwa mwizi namo nyumbani mwake aapaye kiapo cha uwongo na kulitaja Jina langu, nayo itatua katikati ya nyumbani mwake, hata iiangamize yote pamoja na miti yake na mawe yake. Kisha malaika aliyesema na mimi akatoka, akaniambia: Yainue macho yako, uone, kama ndio nini litakalotokea. Nikauliza: Ndio nini? Akasema: Hili ndio pishi kubwa sana linalotokea. Tena akasema: Hili ndio mfano wa watu walioko katika nchi hii yote nzima. Mara nikaona, kifuniko cha risasi kilivyonyanyuliwa, akaonekana mwanamke mmoja aliyekaa ndani ya hilo pishi kubwa, kisha akatupa jiwe la risasi juu ya domo lake. Yule akasema: Huyu ndio uovu; naye akamtupa ndani ya hilo pishi kubwa, kisha akatupa jiwe la risasi juu ya domo lake. Nikayainua macho yangu, nikachungulia mara nikaona, wanawake wawili wakitokea, upepo ukaingia katika mabawa yao, kwani walikuwa na mabawa kama ya korongo, wakalichukua lile pishi kwenda nalo katikati ya nchi na ya mbingu. Nikamwuliza malaika aliyesema na mimi: Hili pishi kubwa hawa wanalipeleka wapi? Akaniambia: Wanakwenda kulijengea nyumba katika nchi ya Sinari; itakapokuwa tayari, yeye mwanamke atawekwa mle ndani mahali pake, alipotengenezewa. Nilipoyainua macho yangu tena, nichungulie, mara nikaona magari manne yaliyotoka katikati ya milima miwili, nayo milima hiyo ilikuwa ya shaba. Gari la kwanza lilikuwa na farasi wekundu, gari la pili lilikuwa na farasi weusi, gari la tatu lilikuwa na farasi weupe, gari la nne lilikuwa na farasi wenye nguvu, miili yao ilikuwa ya madoadoa. Nikaanza kusema na kumwuliza malaika aliyesema na mimi: Hao maana yao nini, Bwana wangu? Malaika akajibu, akaniambia: Hawa ndio pepo nne za mbinguni zinazotaka kutoka sasa kwa kuwa zimekwisha kusimama kwake Bwana wa nchi hii yote nzima. Gari lenye farasi weusi linatoka kwenda katika nchi ya kaskazini, nao weupe wanalifuata. Wale wenye miili ya madoadoa wanatoka kwenda katika nchi ya kusini. Nao wenye nguvu wanatoka kujitafutia mahali pa kwendea, wapate kutembea katika nchi. Alipowaambia: Haya! Nendeni katika nchi! ndipo, walipokwenda kutembea katika nchi. Kisha akapaza sauti na kuniita, akaniambia kwamba: Tazama, hawa wanaotoka kwenda katika nchi ya kaskazini wataituliza roho yangu katika nchi ya kaskazini. Neno la Bwana likanijia la kwamba: Watoze tunzo waliotekwa na kuhamishwa, akina Heldai na Tobia na Yedaya, ukija wewe mwenyewe siku hiyo kuingia nyumbani mwa Yosia, mwana wa Sefania, walimofikia walipotoka Babeli! Tunzo utakalowatoza ni fedha na dhahabu; kisha fanya taji, kamvike mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, kichwani! Umwambie kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema kwamba: Tazama, yuko mtu atakayekuja, jina lake Chipukizi, maana atachipukia mahali pake; ndiye atakayelijenga Jumba la Bwana. Kweli yeye ndiye atakayelijenga Jumba la Bwana na kujipatia utukufu; atakaa katika kiti chake cha kifalme na kutawala, tena atakuwa mtambikaji katika kiti chake cha kifalme, nalo shauri, hao wawili watakalolipiga, litakuwa la mapatano. Nazo hizo taji na zikae katika Jumba la Bwana kuwa ukumbusho wa Helemu na wa Tobia na wa Yedaya na wa Heni, mwana wa Sefania. Nao walioko mbali watakuja kusaidia kulijenga Jumba la Bwana. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa Bwana Mwenye vikosi amenituma kwenu. Haya yatatimia, mkiisikia sauti ya Bwana Mungu wenu na kuitii. Katika mwaka wa nne wa mfalme Dario ndipo, neno la Bwana lilipomjia Zakaria siku ya nne ya mwezi wa Kisilewu ulio wa tisa. Kwani watu wa Beteli walimtuma Sareseri na Regemu-Meleki na watu wao kuja kumnyenyekea Bwana na kuwauliza watambikaji waliomo Nyumbani mwa Bwana Mwenye vikosi na kuwauliza nao wafumbuaji kwamba: Tuomboleze katika mwezi wa tano na kujinyima menginemengine, kama tulivyofanya hii miaka yote iliyopita? *Ndipo, neno la Bwana Mwenye vikosi liliponijia la kwamba: Waambie watu wote wa nchi hii nao watambikaji kwamba: Kama mmefunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba hii miaka 70, je? Mmefunga kwa ajili yangu mimi? Tena kama mnakula au kama mnakunywa, Je? Sio ninyi wenyewe mnaokula, tena mnaokunywa? Yafaayo siyo yale maneno, Bwana aliyoyatangaza vinywani mwa wafumbuji wa kwanza, Yerusalemu ulipokuwa umekaa watu na kutulia vema, navyo vijiji vyake vilipouzunguka, nayo nchi ya kusini ilipokaa watu, hata nchi ya pwani? Neno la Bwana likamjia Zakaria la kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema kwamba: Kateni mashauri ya kweli yaliyo sawa, mhurumiane kila mtu na ndugu yake kwa kuoneana machungu! Wajane nao waliofiwa na wazazi, nao wageni na wanyonge msiwakorofishe, wala mtu na ndugu yake msiwaziane mabaya mioyoni mwenu!* Lakini walikataa kuyasikia hayo, wakawatolea kosi zao ngumu, wakayaziba masikio yao, wasisikie. Wakaishupaza mioyo yao, iwe migumu kama almasi, wasiyasikie Maonyo wala maneno, Bwana Mwenye vikosi aliyoyatuma kwao kwa Roho yake na kuwatumia wafumbuaji wa kwanza. Ndipo, makali mengi yalipowajia toka kwa Bwana Mwenye vikosi. Ikawa hivyo: kama wao walivyokataa kusikia, alipowaita, ndivyo, nami nilivyokataa kuwasikia, waliponiita; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Kwa hiyo nimewatawanya kwa nguvu kama za upepo mkali katika wamizimu wote, wasiowajua, nchi nayo ikageuka nyuma yao kuwa mapori tu, asipatikane mtu aliyeipita wala kwa kwenda wala kwa kurudi. Hivyo ndivyo, walivyoigeuza nchi hii nzuri mno kuwa mapori matupu. Neno la Bwana Mwenye vikosi likanijia la kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Nimeingiwa na wivu mwingi sana kwa ajili ya Sioni, wivu huu ukanitia makali mengi yenye moto kwa ajili yake. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nitarudi Sioni, nikae katikati ya Yerusalemu, nao Yerusalemu utaitwa mji wenye kweli, nao mlima wa Bwana Mwenye vikosi utaitwa mlima mtakatifu. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Itakuwa tena, wazee wa kiume na wa kike wakae katika barabara za Yerusalemu, kila akishika mkongojo mkononi mwake kwa kuwa mzee kabisa. Tena barabara za mji huu zitajaa watoto wa kiume na wa kike watakaocheza palepale barabarani. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Je? Yanayokuwa mambo yasiyowezekana machoni pao walio masao ya ukoo huu yawe napo machoni pangu mambo yasiyowezekana? Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mtaniona, nikiwaokoa walio ukoo wangu na kuwatoa katika nchi ya maawioni kwa jua na katika nchi ya machweoni kwa jua. Kisha nitawaleta, wakae katikati ya Yerusalemu, nao watakuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wao kwa kweli na kwa wongofu. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Itieni mikono yenu nguvu, ninyi mnaoyasikia siku hizi maneno haya vinywani mwa wafumbuaji walioyasema siku hiyo, msingi wa Nyumba ya Bwana Mwenye vikosi ulipowekwa, ijengwe kuwa Jumba lake. Kwani kabla ya siku hizi hakikuwako kitu, watu walichokipata kwa kazi zao, wala hakikuwako, nyama walichokipata kwa kazi zao, tena kwa ajili ya kupingana hawakupata kutengemana wala aliyetoka wala aliyeingia, maana naliwachochea watu wote, wagombane kila mtu na mwenziwe. Lakini sasa mimi sitawaendea walio masao ya ukoo huu, kama nilivyowaendea siku zile za kwanza; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Kwani watapanda na kutengemana: mizabibu itazaa matunda yao, nayo nchi italeta mazao yake, nazo mbingu zitatoa umande wao, basi, hayo yote nitawapa walio masao ya ukoo huu, yawe fungu lao. Kama mlivyokuwa kiapizo kwa wamizimu ninyi mlio mlango wa Yuda nanyi mlio mlango wa Isiraeli, ndivyo, nitakavyowaokoa ninyi, mwe mbaraka; msiogope, ila mikono yenu itieni nguvu! Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kama nilivyowaza moyoni mabaya, nitakayowafanyia ninyi, baba zenu waliponikasirisha, nikaacha kugeuza moyo, ndivyo, nilivyowaza moyoni siku hizi mema, nitakayowafanyia wao wa Yerusalemu nao walio mlango wa Yuda; kwa hiyo msiogope! ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Haya ndiyo maagizo, mtakayoyafanya: Semeni yaliyo kweli kila mtu na mwenziwe, tena kateni malangoni kwenu mashauri yaliyo sawa! Mtu na mwenziwe msiwaziane mabaya mioyoni mwenu, wala msipende kuapa viapo vya uwongo! Kwani hayo yote ndiyo, ninayochukizwa nayo; ndivyo, asemavyo Bwana. Neno la Bwana Mwenye vikosi likanijia la kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mifungo ya mwezi wa nne na wa tano na wa saba na wa kumi itageuka kuwa siku za furaha na za shangwe kwao walio mlango wa Yuda, zitakuwa sikukuu zipendezazo. Lakini sharti myapende mambo ya kweli na matengemano! Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Yako makabila mazima ya watu watakaokuja pamoja na wenyeji wa miji mingi. Wenyeji wa mji mmoja watakwenda kwa wenyeji wa mji mwingine kuwaambia: Haya! Twende kujinyenyekeza mbele ya Bwana na kumtafuta Bwana Mwenye vikosi! Mimi nami nitakwenda. Ndipo, watakapokuja watu wa makabila mengi, hata wamizimu wenye nguvu, wakimtafuta Bwana Mwenye vikosi mle Yerusalemu, wajinyenyekeze mbele ya Bwana. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Siku hizo itakuwa, watu kumi waliotoka katika misemo yote ya wamizimu wamshike mtu mmoja wa Kiyuda wakikamata pindo la nguo yake, kisha watamwambia: Tunataka kwenda nanyi, kwani tumesikia, ya kuwa Mungu yuko pamoja nanyi. Hili ndilo tamko zito la Bwana. linaionya nchi ya Hadiraki na mji wa Damasko, lipate kutua humo, kwani Bwana ndiye, watu wanayemwelekezea macho pamoja na koo zote za Isiraeli. Linaionya nchi ya Hamati inayopakana nao, hata Tiro na Sidoni, kwani ni yenye werevu mwingi ulio wa kweli: Watiro walijijengea boma, wakalimbika fedha, kama ni mavumbi, na dhahabu tupu kama ni taka za barabarani. Lakini mtaona, Bwana akiuteka, azibwage mali zake pamoja na vikosi vyake baharini, lakini wenyewe utateketezwa kwa moto. Askaloni utakapoyaona, utashikwa na woga; nao Gaza utatetemeka sana, Ekroni nao, kwa kuwa mji huo, walioungojea, utakuwa umewatia soni; namo Gaza mfalme atatoweka namo Askaloni hawatakaa watu tena. Asdodi watakaa wana wa ugoni, lakini nitayakomesha majivuno ya Wafilisti. Tena nitaziondoa nyama zao zenye damu vinywani mwao, navyo vyakula vyao vitapishavyo nitaviondoa katika meno yao; ndipo, nao walio masao yao watakapomjua Mungu wetu, wawe kama mkuu kwao Wayuda, nao Waekroni wawe kama Wayebusi. *Kisha nitapiga kambi, iwe kilindo cha Nyumba yangu, pasipite mtu kwenda na kurudi, wala pasipite kwao tena mtesaji, kwani tangu hapo nitawaangalia kwa macho yangu, Piga vigelegele sana, binti Sioni! Shangilia, binti Yerusalemu! Tazama, mfalme wako anakujia! Ni mwongofu na mwokozi, tena ni mnyenyekevu, amepanda punda aliye mwana bado wa kuwa na mama yake. Ndipo, nitakapoyatowesha magari kule Efuraimu, nao farasi mle Yerusalemu, nazo pindi za vita zitatoweshwa, nao wamizimu atawafundisha kutengemana; ufalme wake utaanzia baharini, uifikie bahari ya pili, tena uanzie penye jito kubwa, uyafikie mapeo ya nchi. Wafungwa wako wewe nitawakomboa kwa ajili ya damu ya agano lako, niwatoe shimoni msimo na maji. Rudini ngomeni, ninyi wafungwa mliokishika kingojeo chenu! Leo hivi nawaambia: Nitakurudishia mara mbili yaliyokuwa yako.* Kwani Wayuda ninawatumia kuwa upindi wangu, nao Waefuraimu kuwa mishale; kisha nitawaamsha wanao, Sioni, wawaendee wana wako, Ugriki; ndipo, nitakapokugeuza kuwa kama upanga wa fundi wa vita Naye Bwana ataoneka kwao, mshale wake utokee kama umeme; kisha Bwana Mungu atapiga baragumu akija katika pepo kali za nchi ya kusini. Bwana Mwenye vikosi atawakingia kwa ngao yake, waje kuwala wakiyakanyaga mawe ya makombeo, watakunywa damu zao wakipiga makelele kama wanaokunywa mvinyo; hivyo watajaa kama mabakuli yachukuayo damu za ng'ombe za tambiko, hivyo wenyewe watakuwa kama pembe za meza ya kutambikia. Ndivyo, Bwana Mungu wao atakavyowaokoa siku hiyo, kwa kuwa ndio kundi lao walio ukoo wake, tena ndio vito vya taji vinavyometameta katika nchi yake. Tazameni, wema wao na uzuri wao ulivyokuwa mwingi! Ngano hukuza vijana wa kiume nazo pombe mbichi vijana wa kike. Mwombeni Bwana mvua siku za vuli! Bwana ndiye afanye mawingu yenye umeme; naye ndiye anayewapa matone ya mvua, majani yote ya shambani yaipate. Kwani vinyago husema yasiyo na maana, nao waaguaji huona yaliyo uwongo, husema ndoto zisizo za kweli, wakituliza mioyo, ni bure; kwa hiyo watu hujiendea kama kondoo, huteseka, kwani hakuna awachungaye. Wachungaji ndio, makali yangu yanaowawakia moto, nao viongozi ndio, nitakaowapatiliza; kwani Bwana Mwenye vikosi amelikagua kundi lake, ndio mlango wa Yuda, nao ndio atakaowageuza, wawe kama farasi mwenye utukufu wake katika mapigano. Kwao ndiko, kutakakotoka jiwe la pembeni, hata uwambo wa hema, hata upindi wa kupigania, kweli kwao ndiko, watakakotokea wote pia waongozao vikosi. Nao watakuwa kama mafundi wa vita, wawakanyagao adui matopeni barabarani kwenye mapigano; watakapopigana, Bwana atakuwa nao, wawatweze waliopanda farasi. Nitawatia nguvu walio mlango wa Yuda, nao walio mlango wa Yosefu nitawaokoa, nitawarudisha kwao, kwani nitawahurumia, nao watakuwa kama watu, nisiowatupa kwani mimi Bwana ni Mungu wao, nami nitawaitikia. Nao Waefuraimu watakuwa kama mafundi wa vita, nayo mioyo yao itafurahiwa kama yao waliokunywa mvinyo; wana wao watakapoyaona, watafurahi, nayo mioyo yao itashangilia kwa kuwa na Bwana. Nitawakusanya na kuwapigia miluzi, kwani nitawakomboa; nao watakuwa wengi, kama walivyokuwa wengi kale. Nimewatawanya katika makabila mengine, lakini huko mbali nako watanikumbuka; kwa hiyo watapona pamoja na wana wao, wapate kurudi kwao. Nami nitawarudisha kwao na kuwatoa katika nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika nchi ya Asuri, niwapeleke katika nchi ya Gileadi na ya Libanoni, lakini huko nako hawataenea wote. Watakapopita baharini penye masongano, atayapiga mawimbi pale baharini; ndipo, mafuriko ya maji ya jito la Nili yatakapokupwa yote, nayo majivuno ya Asuri yatanyenyekezwa, nayo bakora ya kifalme ya Misri haitakuwa na budi kutoweka. Nami nitawatia nguvu za kuwa na Bwana, wafanye mwenendo wao katika Jina lake; ndivyo, asemavyo Bwana. Ifungue milango yako, Libanoni, moto uile miangati yako! Ombolezeni, ninyi mivinje, kwa kuwa miangati imeanguka! Miti hiyo iliyokuwa yenye utukufu, imeangamizwa! Ombolezeni, ninyi mivule ya Basani! Kwani msitu uliokuwa hauingiliki umeanguka. Sikilizeni, wachungaji wanavyolia, kwa kuwa hayo malisho yao mazuri mno yameangamizwa! Sikilizeni, wana wa simba wanavyonguruma, kwani machaka ya Yordani, waliyojivunia, yameangamizwa! Hivi ndivyo, Bwana Mungu wangu anavyosema: Wachunge kondoo walio wa kuuawa tu! Waliowanunua huwaua pasipo kukora manza; nao waliowauza husema: Atukuzwe Bwana, kwa kuwa nimepata mali! Nao wachungaji wao hawawahurumii. Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Sitawahurumia tena wakaao katika nchi hii, utaniona, mimi nikiwatoa watu hawa na kuwatia kila mtu mkononi mwa mchungaji wake namo mkononi mwa mfalme wake, ndio watakaoiponda nchi hii, nami sitawaponya mikononi mwao. Basi, nikawachunga hao kondoo walio wa kuuawa tu, nao walikuwa kondoo wanyonge kweli; nikajichukulia fimbo mbili, moja nikaiita Mapendeleo, ya pili nikaiita Mapatanisho, nikawachunga hao kondoo. Nikatowesha wachungaji watatu katika mwezi mmoja, kisha Roho yangu ikashindwa kuwavumilia, roho zao nazo zikanichukia. Nikasema: Sitawachunga ninyi, watakaokufa na wafe! Nao watakaotoweka na watoweke! Nao watakaosalia na walane kila mtu nyama za mwili wa mwenziwe! Kisha nikaichukua fimbo yangu iitwayo Mapendeleo, nikaivunja, ni kwamba: Nilitangue agano langu, nililolifanya na makabila yote. Siku ile, lilipotanguliwa, ndipo, wale kondoo wanyonge walioniangalia walipotambua, ya kuwa hiyo ilifanyika kwa neno la Bwana. Nikawaambia: Mkiona kuwa vema, nipeni mshahara wangu! Kama sivyo, acheni! Wakanipimia fedha 30, ziwe mshahara wangu. Kisha Bwana akaniambia: Mtupie mfinyanzi kima hiki kizuri, walichoniwazia kuwa malipo yangu mimi! Nikazichukua hizo fedha 30, nikazipeleka Nyumbani mwa Bwana, nikamtupia mfinyanzi. Kisha nikaivunja fimbo yangu ya pili iitwayo Mapatanisho, ni kwamba: Niutangue udugu wao Wayuda nao wa Waisiraeli. Bwana akaniambia: Jichukulie tena vyombo vya mchungaji asiyefaa kitu! Kwani utaniona, mimi nikiinua katika nchi hii mchungaji asiyewakagua waliotoweka, asiyewatafuta waliopotea, asiyewaponya waliovunjika, asiyewatunza walio wakiwa, lakini nyama za vinono atazila, nazo kwato zao ataziondoa kwa nguvu. Yatampata huyo mchungaji wangu asiyefaa, anayewaacha kondoo! Upanga utaupiga mkono wake na jicho lake la kuume, mkono wake ukauke kabisa, nalo jicho lake la kuume lipofuke kabisa. Tamko zito la Bwana, alilowaambia Waisiraeli. Ndivyo, asemavyo Bwana aliyezitanda mbingu, aliyeuweka msingi wa nchi, aliyeiumba roho ya mtu ndani yake: Mtaniona, nikiuweka Yerusalemu kuwa chano cha kuwalevya sana wao wa makabila yote wanaokaa na kuuzunguka; hata Wayuda watapatwa na mambo, Yerusalemu utakaposongwa. Siku hiyo ndipo, nitakapouweka Yerusalemu kuwa jiwe zito zaidi lisilochukulika na makabila yote, nao watakaojaribu kulichukua watajiumiza vibaya, ijapo mataifa yote pia ya hapa nchini yaje kukusanyika, yalichukue. Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku hiyo ndipo, nitakapowapiga farasi wote, waingiwe na mastuko, nao wawapandao wapatwe na wazimu; juu yao walio mlango wa Yuda nitayafumbua macho yangu, yawatazame, lakini farasi wote wa makabila ya watu nitawapiga, wapofuke. Ndipo, wakuu wa Yuda watakaposema mioyoni mwao: Wenyeji wa Yerusalemu ndio nguvu zetu, kwa kuwa tunaye Bwana Mwenye vikosi aliye Mungu wake. Siku hiyo ndipo, nitakapowaweka wakuu wa Yuda kuwa kama chetezo cha moto penye kuni na kama mienge ya moto penye miganda mikavu, wapate kuwala kuumeni na kushotoni watu wa makabila yote pia wakaao na kuwazunguka, lakini Yerusalemu utakaa papo hapo mahali pake pa Yerusalemu. Lakini kwanza Bwana atayaokoa mahema ya Yuda, kusudi utukufu wao walio mlango wa Dawidi nao utukufu wao wenyeji wa Yerusalemu usijikuze na kuwabeza Wayuda. Siku hiyo ndipo, Bwana atakapowakingia wenyeji wa Yerusalemu, aliye mnyonge kwao siku hiyo awe kama Dawidi, nao walio wa mlango wa Dawidi wawe kama Mungu, kama malaika wa Bwana awaongozaye. Siku hiyo ndipo, nitakapowatafuta, niwaangamize wamizimu wote wajao kupigana na Yerusalemu. Wao walio wa mlango wa Dawidi nao wenyeji wa Yerusalemu nitawamiminia Roho ya kuhurumiana na ya kuombeana; ndipo, watakaponitazama, waliyemchoma. Kisha wataniombolezea, kama watu wanavyomwombolezea mwana wa pekee, nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama mtu anavyoona uchungu kwa ajili ya mwana aliyezaliwa wa kwanza. Siku hiyo maombolezo yatakuwa mengi mle Yerusalemu, kama maombolezo yalivyokuwa mengi mle Hadadi-Rimoni kule bondeni kwa Megido. Nao wenyeji wa nchi hii wataomboleza kila mlango peke yake: Walio wa mlango wa Dawidi peke yao, nao wanawake wao peke yao, walio wa mlango wa Natani peke yao, nao wanawake wao peke yao. Walio wa mlango wa Lawi peke yao, nao wanawake wao peke yao; walio wa mlango wa Simei peke yao, nao wanawake wao peke yao. Vivyo hivyo milango yote itakayokuwa imesalia, wao wa kila mlango peke yao, nao wanawake peke yao. Siku hiyo ndipo, walio wa mlango wa Dawidi nao wenyeji wa Yerusalemu watakapofunuliwa kisima kwa ajili ya makosa na kwa ajili ya machafu. Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku hiyo ndipo, nitakapoyang'oa majina ya vinyago vyote katika nchi hii, visikumbukwe tena; hata wafumbuaji na roho zenye uchafu nitawaondoa, watoke katika nchi hii. Itakuwa, kama mtu atataka kufumbua maneno tena, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia: Hutapata kuishi, kwani unasema uwongo na kulitaja Jina la Bwana, kisha baba yake na mama yake waliomzaa watamchoma kwa ajili ya ufumbuaji wake. Siku hiyo ndipo, wafumbuaji watakapopatwa na soni, kila mmoja kwa ajili ya maono yake, atakapofumbua maneno, tena hatakuwako atakayevaa joho la manyoya ya nyama, apate kusema yaliyo uwongo. Ila atasema: Mimi si mfumbuaji, mimi ni mtu alimaye shamba, kwani tangu ujana wangu mtu alininunua, niwe mtumwa wake. Mtu atakapomwuliza: Haya makovu kifuani katikati ya mikono yako ni ya nini? atasema: Ni ya mapigo, niliyoyapata nyumbani mwao, niliowapenda. Wewe upanga, amka, umpige mchungaji wangu na mwenzangu wa bia! Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi. Mpige mchungaji, kondoo watawanyike! Nami nitaugeuza mkono wangu, uwaelekeze wadogo. Ndivyo, asemavyo Bwana: Hapo ndipo, mafungu mawili yatakapoangamizwa katika nchi hii yote nzima, yafe, lakini fungu la tatu litasazwa huko. Nalo hilo fungu la tatu nitalitia motoni, niwang'aze kwa kuwayeyusha, kama watu wanavyong'aza fedha kwa kuiyeyusha, tena nitawajaribu kabisa, kama watu wanavyojaribu dhahabu. Kisha hapo, watakapolililia Jina langu, mimi nitawaitikia na kuwaambia: Hawa ndio walio ukoo wangu; ndipo, watakapoitikia wao: Nawe Bwana ndiwe Mungu wetu. Mtaona, siku ya Bwana ikija; ndipo, mateka yako yatakapogawanywa mjini mwako. Kwani nitawakusanya wamizimu wote, waje kuupelekea Yerusalemu vita; ndipo, huo mji utakapochukuliwa, nazo nyumba zitatekwa, hata wanawake watatiwa soni. Kisha nusu ya watu wa mji watatoka humo kwenda utumwani, lakini walio masao ya watu wa humo mjini hawataangamizwa. Kisha Bwana atatoka kupigana nao hao wamizimu, kama alivyopigana nao hata siku nyingine za vita. Siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa michekele ulioko ng'ambo ya Yerusalemu upande wa maawioni kwa jua; ndipo, huo mlima wa michekele utakapopasuka, pawe korongo kubwa sana katikati lielekealo nusu maawioni kwa jua, nusu baharini, kipande kimoja cha mlima huo kikiondoka upande wa kaskazini, kipande chake kingine upande wa kusini. Nanyi mtapata kukimbilia mle bondeni kwenye milima yangu, kwani hilo bonde la milima yangu litakwenda kufika mpaka Aseli; nanyi mtakimbia, kama mlivyoukimbia ule mtetemeko wa nchi siku za Uzia, mfalme wa Yuda. Kisha Bwana Mungu wangu atakuja, nao watakatifu wote watakuwa pamoja na wewe. Siku hiyo haitakuwa na mwanga, nazo nyota zimetukazo zitaguiwa na giza. Siku hiyo moja inayojulikana kwake Bwana haitakuwa mchana wala usiku, lakini wakati wa jioni patakuwa na mwanga tena. Siku hiyo ndipo, maji yenye uzima yatakapotoka Yerusalemu, nusu yatakwenda katika bahari iliyoko maawioni kwa jua, nusu yatakwenda katika bahari nyingine; yatakuwa vivyo hivyo siku za kiangazi na siku za kipupwe. Naye Bwana atakuwa mfalme wa nchi yote nzima tena siku hiyo Bwana atakuwa yeye mmoja, nalo Jina lake litakuwa hilo moja. Nchi yote nzima itageuka kuwa nchi ya tambarare toka Geba hata Rimoni upande wa kusini wa Yerusalemu. Lakini huu wenyewe utatukuka kwa kukaa mahali pake kuanzia penye lango la Benyamini kufikia mahali pa lango la kwanza napo penye lango la pembeni hata mnara wa Hananeli mpaka penye makamulio ya mfalme. Humo ndimo, watu watakamokaa pasipo kupatwa tena na kiapizo cho chote; ndivyo, Yerusalemu utakavyokaa salama. Hili ndilo pigo, Bwana atakaloyapiga makabila yote yaliyopeleka vikosi vyao kupigana na Yerusalemu: ataziozesha nyama za miili yao, wakiwa wamesimama kwa miguu yao, nayo macho yao yataoza ndani ya matundu yao, nazo ndimi zao zitaoza vinywani mwao. Tena siku hiyo ndipo, patakapokuwa kwao kitisho kikubwa kitokacho kwa Bwana, kila mtu akamate mkono wa mwenziwe, nao mkono wake yule utauinukia mkono wa mwenziwe. Wayuda nao watakuja kupigana mle Yerusalemu, mali za wamizimu wote pia wanaokaa na kuuzunguka zitakapokusanywa mle: dhahabu na fedha na nguo za sikukuu nyingi mno. Lile pigo litapiga vilevile nao farasi na nyumbu na ngamia na punda na nyama wote pia watakaokuwamo makambini mwao hao, liwe sawa na pigo lile la watu. Kisha masao ya wamizimu wote waliokuja kupigana na Yerusalemu watatoka kwao kuja kupanda papo hapo mwaka kwa mwaka, wamwangukie mfalme, ndiye Bwana Mwenye vikosi, na kuila sikukuu ya Vibanda. Lakini kama mlango mmoja wa milango ya nchi hautapanda Yerusalemu kumwangukia mfalme, ndiye Bwana Mwenye vikosi, basi, kwao mvua haitanyesha. Ingawa mlango wa Wamisri usipande kufika huko, basi, hata kwao mvua haitanyesha. Hilo ndilo pigo, Bwana atakalowapiga wamizimu watakaokataa kupanda huko, waile sikukuu ya Vibanda. Hilo litakuwa kosa lao Wamisri na kosa lao wamizimu wote watakaokataa kupanda huko, waile sikukuu ya Vibanda. Siku hiyo ndipo, njuga za farasi zitakapokuwa zimeandikwa: Watakatifu wa Bwana. Nazo sufuria zilizomo Nyumbani mwa Bwana zitawaziwa kuwa sawa na vyano vilivyoko penye meza ya kutambikia. Ndipo, kila sufuria iliyomo Yerusalemu au iliyoko katika nchi ya Yuda itakapokuwa takatifu ya Bwana Mwenye vikosi; kwa hiyo wote watakaokuja kutambika watajichukulia moja yao, wajipikie mle nyama ya tambiko. Siku hiyo hatakuwako tena Mkanaani hata mmoja atakayeingia Nyumbani mwa Bwana Mwenye vikosi. Tamko zito la Bwana, alilowaambia Waisiraeli kinywani mwa Malaki. Ndivyo, Bwana anavyosema: Nimewapenda ninyi, nanyi husema: Umetupenda namna gani? Ndivyo, asemavyo Bwana: Je? Esau siye kaka yake Yakobo? Nami nilimpenda Yakobo. Lakini Esau nilimchukia, milima yake nikaigeuza kuwa mapori matupu, nalo fungu lake nikawapa mbwa wa nyikani. Sasa Edomu akisema: Tumepondwa, lakini tutayajenga tena mabomoko, Bwana Mwenye vikosi atawajibu: Ijapo wao wajenge, mimi nitajengua, nao watu watawaita: Nchi yao wasiomcha Mungu, tena: Ukoo wao, Bwana anaowakasirikia kale na kale. Macho yenu yatayaona, nanyi mtasema: Bwana hutukuka kuipita mipaka ya Isiraeli. Mwana humheshimu baba yake, hata mtumwa humheshimu bwana wake; kama mimi na Baba yenu, heshima yangu iko wapi? Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyowauliza ninyi watambikaji mnaolibeza Jina langu, kisha mnasema: Jina lako tumelibeza kwa nini? Ninyi huleta mezani pangu pa kutambikia vilaji vya tambiko vichafu na kusema: Tumekutia uchafu kwa nini? Ni kwa kusema kwenu: Meza ya Bwana hubezeka. Tena mkileta nyma kipofu kuwa ng'ombe ya tambiko, si vibaya? Au mkileta achechemeaye au aliyeugua, si vibaya? Haya! Umpelekee mtawala nchi vyako vilivyo hivyo, uone, kama atapendezwa na wewe, akupendelee! ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Sasa ulalamikieni uso wa Mungu, atuhurumie! Ikiwa vipaji kama hivyo vimetolewa na mikono yenu, je? Atawapendelea? Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Vingekuwa vyema, kama mtu wa kwenu angeifunga milango, msije kuwasha moto bure mezani pangu pa kutambikia! Sipendezwi kabisa nanyi, wala sipendezwi na vipaji vya tambiko vitokavyo mikononi mwenu; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Kwani kutoka maawioni kwa jua mpaka machweoni kwake Jina langu ni kuu kwa wamizimu, tena kila mahali Jina langu linatolewa mavukizo na vipaji vya tambiko vitakatavyo, kwani Jina langu ni kuu kwa wamizimu; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Lakini ninyi hulipatia uchafu kwa kusema kwenu: Meza ya Bwana hubezeka, nayo inayotupatia ni chakula kinachobeuliwa. Tena anasema Bwana Mwenye vikosi: Mwasema: Tazameni, tunavyosumbuka! kisha mwazinung'unikia kazi zenu na kuleta nyama aliyenyang'anywa au achechemeaye au auguaye, mmtoe kuwa ng'ombe ya tambiko; basi, nipendezwe na vipaji hivyo vitokavyo mikononi mwenu? ndivyo, Bwana anavyosema. Na awe ameapizwa huyu mdanganyifu anayekuwa na nyama wa kiume katika kundi lake! Lakini akiapa kutoa mmoja, anapeleka aliye mbaya kumchinjia Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko. Kwani mimi ni mfalme mkuu, nalo Jina langu huogopwa kwa wamizimu; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Sasa ninyi watambikaji, agizo hili mnatolewa ninyi. Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Msiposikia, wala msipoyatia mioyoni mwenu, mlipe Jina langu macheo, ndipo, nitakapowaapiza ninyi, nazo mbaraka zenu nitazigeuza kuwa maapizo; hata sasa nimekwisha kuzigeuza kuwa maapizo, kwani ninyi hamyatii haya mioyoni mwenu. Mtaniona, nikiyakemea mazao yenu ninyi, nikiwatupia mavi usoni penu, na yale mavi ya ng'ombe za tambiko za sikukuu zenu, nao watu watawachukua ninyi, wawapeleke penye hayo mavi. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa nimewatolea agizo hili, liwe agano langu, nitakalolifanya na Lawi; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Agano langu, nililolifanya naye, lilikuwa la kumpatia uzima na utengemano; naye ndiye, niliyempa, aniogope; akaniogopa kweli, akajinyenyekeza mbele ya Jina langu. Maonyo ya kweli yalikuwa kinywani mwake, lakini uovu haukuonekana midomoni mwake, akendelea kufuatana na mimi kwa utengemano na kwa unyofu, akarudisha wengi, wasiufuate uovu. Kwani midomo ya mtambikaji sharti iangalie yaliyo yenye ujuzi, nayo Maonyo ndiyo, watu wanayoyatafuta kinywani mwake, kwani yeye ni mjumbe wa Bwana Mwenye vikosi. Lakini ninyi mmeiacha njia hiyo, mkakwaza wengi, wasiyashike Maonyo, mkalivunja agano, nililolifanya na Lawi; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Kwa hiyo mimi nami nimewatoa ninyi, mbezwe nao wote walio wa ukoo huu na kunyenyekezwa vivyo hivyo, kama ninyi mlivyokataa kuzishika njia zangu, mkawapendelea watu mlipowafundisha Maonyo. Je? Sisi sote baba yetu si mmoja? Kumbe aliyetuumba si yeye Mungu mmoja? Mbona tunaendeana kwa udanganyifu kila mtu na ndugu yake, tulipatie uchafu agano la baba zetu? Wayuda ni wadanganyifu, yafanyikayo kwao Waisiraeli namo Yerusalemu ni matendo yatapishayo, kwani Wayuda wamepachafua Patakatifu pa Bwana, anapopapenda, walipooa wanawake wa mungu mgeni. Mtu afanyaye hayo Bwana na amwangamize mahemani mwa Yakobo, mfunzi na mwanafunzi naye ampelekeaye Bwana Mwenye vikosi vipaji vya tambiko! Tena hili ni la pili mnalolifanya: meza ya kumtambikia Bwana mnaifunika kwa machozi yao wamliliao na kupiga kite, asitazame tena kipaji cho chote cha tambiko, wala asipokee mikononi mwenu cho chote cha kumpendeza. Nanyi mnauliza: Kwa sababu gani? Ni kwa sababu Bwana ni shahidi wako na shahidi wa mkeo wa ujana wako, uliyemwacha wewe kwa kumdanganya, naye alikuwa mwenzako wa kabila na mke wako wa kuagana naye. Hakuna mtu hata mmoja anayeweza kufanya hayo akiwa analo bado sao la kiroho. Naye yule mmoja alifanya nini? Alitafuta mzao wa Mungu! Kwa hiyo jiangalieni rohoni mwenu, msiwadanganye wake zenu wa ujana wenu! Kwani Bwana Mungu wa Isiraeli anasema: Ninachukia kuachana, maana ni kuyafunika mavazi yao kwa ukorofi; ndivyo, anavyosema Bwana Mwenye vikosi; kwa hiyo jiangalieni rohoni mwenu, msidanganye! Mmemchokesha Bwana kwa maneno yenu, mkiuliza: Tumemchokesha kwa nini? Ni kwa kusema kwenu; kila afanyaye mabaya ni mwema machoni pa Bwana, nao walio hivyo ndio, anaopendezwa nao! Au mkiuliza: Yuko wapi Mungu anayepatiliza? Mtaniona, nikimtuma mjumbe wangu, atengeneze njia mbele yangu. Yule Bwana, mnayemtafuta, atakuja kutokea Jumbani mwake, msipomwazia. Naye mjumbe wa agano anayewapendeza mtamwona, anavyokuja; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Lakini yuko nani atakayeivumilia siku ya kuja kwake? Tena yuko nani atakayesimama, atakapoonekana? Kwani yeye ni kama moto wa mwenye kuyeyusha fedha au kama sabuni ya wafua nguo. Naye atakaa akiyeyusha fedha, aitakase; ndivyo, atakavyowatakasa wana wa Lawi, awang'aze, wawe kama dhahabu au fedha, wapate kumpelekea Bwana vipaji vya tambiko kwa wongofu. Ndipo, vipaji vya tambiko vya Yuda na vya Yerusalemu vitakapompendeza Bwana kama katika siku za kale na kama katika miaka iliyopita zamani. Hapo ndipo, nitakapowatokea kukata mashauri, nami nitakuwa shahidi wa kuwasuta wachawi na wavunja unyumba, nao waapao viapo vya uwongo, nao wawanyimao wakibarua mshahara, nao wakorofishao wajane hata waliofiwa na wazazi, nao wapotoao wageni pasipo kuniogopa mimi; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.* Kwani mimi Bwana sikugeuka, nanyi hamkukoma kuwa wana wa Yakobo. Tangu siku za baba zenu mmeyaacha maongozi yangu, hamkuyashika, myaangalie. Rudini kwangu! Ndipo, nami nitakaporudi kwenu; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Nanyi mnauliza: Turudi kwa njia gani? Je? Mtu anaweza kumnyima Mungu yaliyo yake? Kwani ninyi mnaninyima yaliyo yangu, mkisema: Tumekunyima namna gani yaliyo yako? Ni mafungu ya kumi na vipaji vya kupatolea Patakatifu. Ninyi mmekwisha kuapizwa kwa kiapizo, tena ninyi mmeninyima yaliyo yangu, taifa hili lote. Yapelekeni mafungu yote ya kumi mle nyumbani, kilimbiko kilimo, yawe vilaji vya Nyumbani mwangu! Kanijaribuni hivyo, kama sitawafunulia madirisha ya mbinguni, nikiwamwagia mbaraka isiyopimika kwa kufurika; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Ndipo, nitakapowakemea walafi kwa ajili yenu, wasiwaangamizie mazao ya nchi, wala mizabibu yenu iliyoko mashambani isikose matunda; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Ndipo, wamizimu wote watakapowatukuza kuwa wenye shangwe, kwani mtakuwa nchi ipendezayo; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Maneno yenu, mliyoyasema kwa ajili yangu, yamekuwa magumu; ndivyo, Bwana anavyosema, nanyi mkauliza: Tumesema nini kwa ajili yako wewe? Mmesema: Ni bure kumtumikia Mungu, tumejipatia nini kwa kuyaangalia maagizo yake yaliyotupasa kuyaangalia na kwa kumwendea Bwana Mwenye vikosi na kuvaa nguo za matanga? Kwa hiyo sasa tunawawazia wao wasiomkumbuka Mungu kuwa wenye shangwe, hata wao wasiomcha Mungu wamejengwa, napo hapo, walipomjaribu Mungu, wamepona. Hapo, wamchao Bwana walipoongeana kila mtu na mwenziwe, Bwana alitega sikio, akasikiliza; mbele yake kikaandikwa kitabu cha ukumbusho wao waliomcha Bwana na kulikumbuka Jina lake. Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi asemavyo: Hao watakuwa wangu mimi mwenyewe siku hiyo nitakayoifanya mimi, nami nitawahurumia, kama mtu anavyomhurumia mwanawe aliyemtumikia. Hapo ndipo, mtakapoona tena, ya kuwa wanapambanuka amchaye Bwana naye asiyemcha, tena amtumikiaye Mungu naye asiyemtumikia. *Kwani mtaiona hiyo siku, ikija na kuwaka moto kama wa tanuru; ndipo, waliomsahau Mungu nao wote waliofanya maovu watakapokuwa makapi, siku hiyo ijayo itakapoyateketeza, isisaze wala mizizi wala matawi yao hao; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Lakini ninyi mliogopao Jina langu jua la wongofu litawachea, nalo litakuwa linao uponya mabawani mwake; ndipo, mtakapochezacheza kama ndama watokao zizini. Nao wasiomcha Bwana mtawaponda na kuwakanyagakanyaga, kwani watageuka kuwa uvumbi chini ya nyayo za miguu yenu siku hiyo, nitakayoifanya mimi. Yakumbukeni Maonyo ya mtumishi wangu Mose, niliyomwagiza kule Horebu, awafundishe Waisiraeli wote maongozi na maagizo. Na mwone, nikimtuma mfumbuaji Elia kuja kwenu, siku kubwa ya Bwana iogopeshayo itakapokuwa haijatimia bado. Yeye ndiye atakayeigeuza mioyo ya baba, warudi kwa watoto, nayo ya watoto, warudi kwa baba zao, nisije kuipiga nchi na kuiapiza.* Chuo cha uzao wake Yesu Kristo, mwana wa Dawidi, mwana wa Aburahamu, ni hiki: Aburahamu alimzaa Isaka, Isaka akamzaa Yakobo, Yakobo akamzaa Yuda na nduguze, Yuda na Tamari wakamzaa Peresi na Zera, Peresi akamzaa Hesiromu, Hesiromu akamzaa Ramu, Ramu akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nasoni, Nasoni akamzaa Salmoni. Salmoni na Rahabu wakamzaa Boazi, Boazi na Ruti wakamzaa Obedi, Obedi akamzaa Isai, Isai akamzaa mfalme Dawidi. Dawidi na mkewe Uria wakamzaa Salomo, Salomo akamzaa Rehabeamu, Rehabeamu akamzaa Abia, Abia akamzaa Asafu, Asafu akamzaa Yosafati, Yosafati akamzaa Yoramu, Yoramu akamzaa Uzia, Uzia akamzaa Yotamu, Yotamu akamzaa Ahazi, Ahazi akamzaa Hizikia, Hizikia akamzaa Manase, Manase akamzaa Amoni, Amoni akamzaa Yosia, Yosia akamzaa Yekonia na nduguze siku zile, walipohamishwa kwenda Babeli. Walipokwisha kuhamishwa kwenda Babeli, Yekonia akamzaa Saltieli, Saltieli akamzaa Zerubabeli, Zerubabeli akamzaa Abihudi, Abihudi akamzaa Eliakimu, Eliakimu akamzaa Azoro, Azoro akamzaa Sadoko, Sadoko akamzaa Ahimu, Ahimu akamzaa Elihudi, Elihudi akamzaa Elazari, Elazari akamzaa Matani, Matani akamzaa Yakobo, Yakobo akamzaa Yosefu, mumewe Maria aliyekuwa mama yake Yesu aitwaye Kristo. Basi, vizazi vyote tangu Aburahamu mpaka Dawidi ni vizazi 14; tangu Dawidi mpaka kuhamishwa kwenda Babeli ni vizazi 14, tena tangu kuhamishwa kwenda Babeli mpaka Kristo ni vizazi 14. Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria, mama yake, alionekana ana mimba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu hapo, alipokuwa ameposwa na Yosefu, nao walikuwa hawajakaribiana. Yosefu, mchumba wake, alikuwa mwongofu, tena hakutaka kumwumbua, kwa hiyo alitaka kumwacha tu, watu wasijue. Alipokuwa akiyafikiri haya, mara malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto akisema: Yosefu, mwana wa Dawidi, usiogope kumwoa Maria, Mchumba wako, kwani kitakachozaliwa naye ni cha Roho Mtakatifu. Atazaa mtoto mwanamume, naye utamwita jina lake Yesu. Kwani yeye ndiye atakayewaokoa watu wake katika makosa yao. Haya yote yalifanyika, lipate kutimia lililonenwa na Bwana kwa mfumbuaji: Tazama, mwanamwali atapata mimba, atazaa mtoto mwanamume, nalo jina lake watamwita Imanueli, ni kwamba: Mungu yuko nasi.* Yosefu alipoamka katika usingizi akatenda, kama malaika wa Bwana alivyomwagiza. Akamwoa mchumba wake, lakini hakumkaribia, mpaka alipomzaa mwanawe wa kwanza. Akamwita jina lake YESU. Yesu alipokwisha kuzaliwa Bet-Lehemu wa Uyuda wakati wa mfalme Herode, ndipo, walipofika Yerusalemu wachunguza nyota waliotoka upande wa maawioni kwa jua. Wakasema: Yuko wapi aliyezaliwa kuwa mfalme wa Wayuda? Kwani tumeiona nyota yake katika nchi ya maawioni kwa jua, basi, tumekuja kumwangukia. Mfalme Herode alipoyasikia haya akahangaika, nao Yerusalemu wote pamoja naye. Akawakusanya wote waliokuwa watambikaji wakuu na waandishi wa kwao akapeleleza kwao mahali, Kristo atakapozaliwa. Nao wakamwambia: Atazaliwa Beti-Lehemu wa Uyuda, kwani ndivyo, alivyoandika mfumbuaji: Nawe Beti-Lehemu wa nchi ya Yuda, hu mdogo kamwe katika majumbe ya Yuda. Kwani mwako ndimo, atakamotoka mtawala atakayewachunga walio ukoo wangu wa Isiraeli. Kisha Herode akawaita wale wachunguza nyota na kufichaficha, akazidi kuwauliza vema siku, ile nyota ilipooneka. Akawatuma Beti-Lehemu akisema: Nendeni, mkapeleleze sana habari za mtoto huyo! Mtakapomwona mnipashe habari, nami nipate kwenda nimwangukie. Nao walipokwisha msikia mfalme wakashika njia. Walipotazama, ile nyota, waliyoiona maawioni kwa jua, ikawatangulia, mpaka ikaja kusimama juu sawa ya mle alimokuwa yule mtoto. Walipoiona hiyo nyota wakafurahi furaha kubwa mno. Wakaingia nyumbani mle, wakamwona mtoto pamoja na mama yake Maria, wakamwangukia na kumnyenyekea. Walipokwisha wakayafungua malimbiko yao, wakamtolea mtoto tunu, dhahabu na uvumba na manemane. Nao walipoonywa kwa ndoto, wasimrudie Herode, wakashika njia nyingine, wakaenda kwao.* Hao walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akisema: Inuka, mchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukakae huko, mpaka nitakapokuambia! Kwani Herode atamtafuta mtoto, amwangamize. Kisha akainuka, akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda Misri. Akakaa huko, mpaka Herode alipokwisha kufa, lipata kutimia neno, Bwana alilolisema kwa mfumbuaji: Misri ndiko, nilikomwitia mwanangu. Herode alipoona, ya kuwa wale wachunguza nyota wamemdanganya akakasirika sana, akatuma watu, wawaue watoto waume wote waliokuwako Beti-Lehemu na vilimani pake pote, waliokuwa wa miaka miwili nao waliopungua, kama alivyoipeleleza siku kwao wachunguza nyota. Ndipo, lilipotimia lililosemwa na mfumbuaji Yeremia kwamba: Sauti imesikiwa Rama, ni kilio na maombolezo mengi. Raheli anawalilia watoto wake, hakutaka kubembelezwa, kwani hawako. Herode alipokwisha kufa, mara malaika wa Bwana akamtokea Yosefu kwa ndoto huko Misri, akamwambia: Inuka, umchukue mtoto na mama yake, uende katika nchi ya Isiraeli! Kwani wamekwisha kufa waliotafuta kumwua mtoto. Ndipo, alipoinuka, akamchukua mtoto na mama yake, akaiingia nchi ya Isiraeli. Lakini aliposikia, ya kuwa Arkelao ametawala Yudea mahali pa Herode, baba yake, akaogopa kwenda huko. Basi akaagizwa kwa ndoto, aende zake pande za Galilea; kwa hiyo akaja, akakaa mji uitwao Nasareti, lipate kutimia lililosemwa na wafumbuaji: Ataitwa Mnasareti.* Siku zile alitokea Yohana Mbatizaji, akapiga mbiu nyikani kwa Yudea akisema: Juteni! Kwani ufalme wa mbinguni umekaribia. Kwani huyo ndiye, aliyemtaja mfumbuaji Yesaya aliposema: Iko sauti ya mtu apigaye mbiu nyikani: Itengenezeni njia ya Bwana! Yanyosheni mapito yake! Naye Yohana alikuwa amevaa mavazi ya manyoya ya ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni pake; chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Ndipo, walipomtokea wa Yerusalemu, nao wote wa Yudea na wa nchi zote za kando ya Yordani, wakabatizwa naye katika mto wa Yordani wakiyaungama makosa yao. Lakini alipoona, Mafariseo na Masadukeo wengi wakimjia, wabatizwe, akawaambia: Ninyi wana wa nyoka, nani aliwaambia ninyi ya kuwa mtayakimbia makali yatakayokuja? Tendeni mazao yaliyo ya kujuta kweli! Msiwaze mioyoni mwenu kusema: Tunaye baba yetu, ndiye Aburahamu! Kwani nawaambiani: katika mawe haya ndimo, Mungu awezamo kumwinulia Aburahamu wana. Miti imekwisha wekewa mashoka mashinani, kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa, utupwe motoni. Mimi nawabatiza katika maji, mpate kujuta. Lakini yeye anayekuja nyuma yangu ana nguvu kunipita mimi, nami sifai kumchukulia viatu vyake. Yeye atawabatiza katika Roho takatifu na katika moto.* Ungo wa kupepetea umo mkononi mwake, naye atapafagia pake pa kupuria ngano. Ngano zake atazikusanya, aziweke chanjani, lakini makapi atayachoma kwa moto usiozimika. Ndipo, Yesu alipotoka Galilea, akafika Yordani, akamjia Yohana akitaka kubatizwa naye. Lakini Yohana akamzuia akisema: Mimi imenipasa kubatizwa na wewe, nawe wewe unanijia mimi? Yesu akajibu akimwambia: Acha tu! Kwani ndivyo, inavyotupasa kuyatimiza maongozi yote. Ndipo, alipomwachia. Yesu alipokwisha batizwa, papo hapo, alipotoka majini, mbingu zikafunuka, akaona, Roho ya Mungu anavyoshuka kama njiwa na kumjia yeye. Mara sauti ikatoka mbinguni ikasema: Huyu ndiye mwanangu mpendwa, ambaye nimependezwa naye.* Kisha Yesu akapelekwa na Roho nyikani, ajaribiwe na Msengenyaji. Akafunga siku 40 mchana na usiku, kisha akaona njaa. Mjaribu akamjia, akamwambia: Kama ndiwe Mwana wa Mungu, yaambie mawe haya, yawe chakula! Naye akamjibu: Imeandikwa: Mtu hataishi kwa chakula tu, ila kwa kila neno linalotoka kinywani mwa Mungu. Kisha Msengenyaji akampeleka katika mji mtakatifu, akamsimamisha juu pembeni hapo Patakatifu, akamwambia: Kama ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini! Kwani imeandikwa: Atakuagizia malaika zake, nao wakakuchukua mikononi mwao usije kujikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia: Tena imeandikwa: Usimjaribu Bwana Mungu wako! Kisha Msengenyaji akampeleka, akampandisha mlima mrefu sana, akamwonyesha ufalme wote pia wa ulimwengu huu na utukufu wake, akamwambia: Haya yote nitakupa, ukiniangukia na kuninyenyekea. Hapo Yesu akamwambia: Nenda zako, Satani! Kwani imeandikwa: Umwangukie Bwana Mungu wako na kumtumikia peke yake! Ndipo, Msengenyaji alipomwacha. Mara malaika wakaja, wakamtumikia.* Yesu aliposikia, ya kwamba Yohana amefungwa, akaondoka akaenda mpaka Galilea. Akahama Nasareti, akaenda kukaa Kapernaumu ulioko pwani mipakani kwa Zebuluni na Nafutali, kusudi neno, mfumbuaji Yesaya alilolisema, lipate kutimizwa: Nchi ya Zebuluni na nchi ya Nafutali zilizoko upande wa pwani na ng'ambo ya Yordani, Galilea ya wamizimu iliko, huko watu waliokaa gizani wameona mwanga mkuu, waliokaa penye kivuli kuacho mwanga umemulika juu yao. Tangu hapo ndipo, Yesu alipoanzia kupiga mbiu akisema: Juteni! Kwani ufalme wa mbingu umekaribia. Basi, Yesu alipokuwa akitembea kandokando ya bahari ya Galilea akaona watu wawili waliokuwa ndugu, ni Simoni aitwaye Petero na nduguye, Anderea. Aliwaona, wakitupa nyavu zao baharini, kwani walikuwa wavuvi. Akawaambia: Njoni, mnifuate! Nami nitawafanya kuwa wavua watu. Papo hapo wakaziacha nyavu, wakamfuata. Alipoendelea mbele, akaona wengine wawili walikuwa ndugu, ni Yakobo wa Zebedeo na nduguye, Yohana. Aliwaona pamoja na baba yao Zebedeo chomboni, wakizitengeneza nyavu zao, akawaita. Papo hapo wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata. Yesu akazunguka katika nchi yote ya Galilea, akawafundisha katika nyumba zao za kuombea, akautangaza Utume mwema wa ufalme na kuwaponya watu wote waliokuwa wagonjwa na wanyonge. Uvumi wake ukaienea nchi yote ya Ushami. Wakampelekea wote walikuwa hawawezi, walioshikwa na magonjwa na maumivu yo yote, nao wote waliokuwa wenye pepo na wenye kifafa na wenye kupooza, naye akawaponya. Wakamfuata makundi mengi ya watu waliotoka Galilea na upande wa ile Miji Kumi na Yerusalemu na Yudea na ng'ambo ya Yordani. *Alipoyaona hayo makundi ya watu akapanda mlimani, akakaa, nao wanafunzi wake wakamkaribia. Ndipo, alipokifumbua kinywa chake, akawafundisha akisema: Wenye shangwe ndio walio maskini rohoni mwao, maana hao ufalme wa mbingu ni wao. Wenye shangwe ndio wanaosikitika, maana hao watatulizwa. Wenye shangwe ndio wapole, maana hao watairithi nchi. Wenye shangwe ndio wenye njaa na kiu ya kupata wongofu, maana hao watashibishwa. Wenye shangwe ndio wenye huruma, maana hao watahurumiwa. Wenye shangwe ndio waliotakata mioyoni mwao, maana hao watamwona Mungu. Wenye shangwe ndio wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu. Wenye shangwe ndio wanaofukuzwa kwa ajili ya wongofu wao, maana hao ufalme wa mbingu ni wao. Nanyi mtakuwa wenye shangwe, watu watakapowatukana na kuwafukuza na kuwasingizia maneno mabaya yo yote yaliyo ya uwongo kwa ajili yangu mimi. Furahini na kushangilia! Kwani mshahara wenu ni mwingi mbinguni. Kwani ndivyo, walivyowafukuza wafumbuaji waliowatangulia.* *Ninyi m chumvi ya nchi. Lakini chumvi ikiwa imepotewa na ukolezi, itatiwa kitu gani, ipate kukolea tena? Hakuna kitu tena, ilichokifalia, itatupwa tu nje, ikanyagwe na watu. Ninyi m mwanga wa ulimwengu. Mji ukiwa juu ya mlima haufichiki. Nao watu wakiwasha taa hawaiweki chini ya kapu, ila huiweka juu ya mwango; ndivyo inavyowaangazia wote waliomo nyumbani. Vivyo mwanga wenu uangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu alioko mbinguni.* Msiniwazie, ya kuwa nimejia kuyatangua Maonyo au maneno ya Wafumbuaji. Sikujia kutangua, nimejia kutimiza. Kweli nawaambiani: Mpaka hapo, mbingu na nchi zitakapokoma, hata kiandiko kimoja au kichoro kimoja kilichomo katika Maonyo hakitakoma, isipokuwa yametimizwa yote. Mtu akiondoa moja tu katika maagizo hayo, ijapo liwe dogo, na kufundisha watu hivyo, huyo ataitwa mdogo kuliko wote katika ufalme wa mbingu; lakini mtu akiyafanya maagizo hayo na kufundisha watu hivyo, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbingu. Kwani nawaambiani: *Wongofu wenu usipoupita wongofu wao waandishi na Mafariseo, hamtaingia kabisa katika ufalme wa mbingu. Mmesikia, ya kuwa watu wa kale waliambiwa: Usiue! Mtu akiua, itampasa, ahukumiwe. Lakini mimi nawaambiani: Kila anayemwonea ndugu yake chuki, itampasa, ahukumiwe. Naye atakayemwambia ndugu yake: Mshenzi wee! itampasa, ahukumiwe na baraza ya wakuu wote. Lakini atakayemtukana ndugu yake, itampasa, atupwe shimoni mwa moto. Ukipeleka kipaji chako mezani pa Bwana, ukakumbuka hapo, ya kuwa ndugu yako ana mfundo moyoni kwa ajili yako, basi, kwanza kiache kipaji chako mbele ya meza ya Bwana! Uende kwanza, upatane na ndugu yako! Kisha urudi, ukitoe kipaji chako! Umwitikie mshtaki wako upesi ukiwa naye, mngaliko njiani! Maana mshtaki wako asikupeleke kwa mwenye hukumu, naye mwenye hukumu asikutie mkononi mwa askari, ukatiwa kifungoni. Kweli nakuambia: Hutatoka humo kabisa, mpaka utakapomaliza kulipa, isisalie hata senti moja* Mmesikia ya kuwa ilisemwa: Usizini! Lakini mimi nawaambiani: Kila mtu anayetazama mwanamke kwa kumtamani, basi, huyo amekwisha zini naye moyoni mwake. Nawe kama jicho lako la kuume linakukwaza, ling'oe, ulitupe mbali! kwani itakufaa, kiungo kimoja tu kiangamie, kuliko mwili wako mzima ukitupwa shimoni mwa moto. Nawe kama mkono wako wa kuume unakukwaza, uukate, uutupe mbali! Kwani itakufaa, kiungo kimoja tu kiangamie, kuliko mwili wako mzima ukijiendea shimoni mwa moto. Tena ilisemwa: Mtu akimwacha mkewe ampe cheti cha kuachana. Lakini mimi nawaambiani: kila mtu anayemwacha mkewe, isipokuwa kwa ajili ya ugoni, huyo anamzinisha. Naye atakayeoa mke aliyeachwa anazini. Tena mmesikia, ya kuwa watu wa kale waliambiwa: Usiape kiapo cha uwongo, lakini umtimizie Mungu, uliyomwapia! Lakini mimi nawaambiani: Usiape na kutaja yoyote, wala mbingu, kwani ndicho kiti cha kifalme cha Mungu; Wala nchi, kwani ndipo pa kuiwekea miguu yake; wala Yerusalemu, kwani ndio mji wa mfalme aliye mkuu; wala kichwa chako, kwani hata unywele mmoja tu huwezi kuugeuza uwe mweupe au mweusi. Mkisema: Ndio, iwe ndio kweli! Au mkisema: Sio, iwe sio kweli! Lakini yanayoyapita hayo hutoka kwa Mbaya. Mmesikia, ya kuwa ilisemwa: Jicho kwa jicho, jino kwa jino! Lakini mimi nawaambiani: Msibishane na mbaya! Lakini mtu akikupiga kofi shavu la kuume, mgeuzie la pili, alipige nalo! Mtu akitaka kushtakiana na wewe, apate kuichukua shuka yako, basi, umwachie na kanzu! Naye atakayekushurutiza kwenda naye nusu saa, basi, nenda naye saa nzima! Anayekuomba umpe, naye anayetaka kukopa kwako usimgeukie mgongo! Mmesikie, ya kuwa ilisemwa: Umpende mwenzio, naye adui yako umchukie! Lakini mimi nawaambiani: Wapendeni adui zenu! Wabarikini wanaowaapiza! Wafanyieni mazuri wanaowachukia! Waombeeni wanaowachokoza na kuwafukuza! Fanyeni hivi, mpate kuwa wana wa Baba yenu alioko mbinguni! Kwani yeye huwacheshea jua lake wabaya na wema, tena huwanyeshea mvua waongofu nao wapotovu. Kwani mkiwapenda wanaowapendani mtapata mshahara gani? Je? Hata watoza kodi hawafanyi hivyo hivyo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu mnawapitaje wengine? Je? Hata wamizimu hawafanyi vivyo hivyo? Basi, ninyi mwe watimilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mtimilifu! Angalieni, msigawie watu vipaji vyenu machoni pa watu, kwamba wawaone! Msipojiangalia hivyo, hamna mshahara kwa Baba yenu alioko mbinguni. Basi, ukimgawia mtu usipigishe baragumu mbele yako kama wanavyofanya wajanja katika nyumba za kuombea na katika njia za mijini, wapate kutukuzwa na watu. Kweli nawaambiani: wamekwisha upata mshahara wao. Lakini wewe ukimgawia mtu, mkono wako wa kushoto usitambue, wa kuume unayoyafanya, huko kugawa kwako kuwe kumejificha! Ndipo, Baba yako anayeyaona hata yanayojificha atakapokulipa waziwazi. Tena mnapomwomba Mungu msiwe kama wajanja! Kwani wanapenda kuomba wakisimama katika nyumba za kuombea na pembeni pa njia za mijini, watu wapate kuwaona. Kweli nawaambiani: wamekwisha upata mshahara wao. Lakini wewe unapoomba uingie mwako chumba cha ndani na kuufunga mlango wako! Kisha umwombe Baba yako alioko fichoni! Ndipo, Baba yako anayeyaona hata yanayojificha atakapokulipa waziwazi. Tena mnapoomba msijisemee maneno tu kama wamizimu! Kwani hudhani, ya kuwa maneno yao mengi yatawapatia kusikilizwa. Msifanane nao! Kwani Baba yenu anayajua yanayowapasa, mnapokuwa hamjamwomba. Ninyi mnapoomba mwombe hivi: Baba yetu ulioko mbinguni, Jina lako litakaswe! Ufalme wako uje! Uyatakayo yatimizwe nchini, kama yanavyotimizwa mbinguni! Tupe leo chakula chetu cha kututunza! Tuondolee makosa yetu, kama nasi tulivyowaondolea waliotukosea! Usituingize majaribuni! Ila tuokoe maovuni! Kwani wako ni ufalme na nguvu na utukufu kale na kale. Amin. Kwani ninyi mnapowaondolea watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawandolea ninyi vilevile. Lakini ninyi msipowaondolea watu makosa yao, hata Baba yenu hatawaondolea ninyi makosa yenu. Tena mnapofunga msikunjamane nyuso kama wajanja! Kwani huzirembua nyuso, kusudi watu wawaone, wanavyofunga. Kweli nawaambiani: Wamekwisha upata mshahara wao. Lakini wewe unapofunga jipake kichwa chako mafuta, unawe nao uso wako, kusudi watu wasikuone, ya kama unafunga, ila akuone Baba yako alioko fichoni. Ndipo, Baba yako anayeyaona yanayojificha atakapokulipa. Msijilimbikie malimbiko nchini, mende na kutu zinapoyaharibu! Nao wezi huyafukua na kwiba. Lakini jilimbikieni malimbiko mbinguni, yasikoharibiwa na mende wala na kutu, wala wezi wasikoyafukua na kwiba! Kwani limbiko lako liliko, ndiko, nao moyo wako utakakokuwa. Taa ya mwili ni jicho. Basi jicho lako liking'aa, mwili wako wote utakuwa na mwanga. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi, mwanga uliomo ndani yako unapokuwa giza, giza yenyewe itakuwaje? *Hakuna mtu anayeweza kutumikia mabwana wawili. Kwani itakuwa hivi: atamchukia wa kwanza na kumpenda wa pili, au atashikamana naye wa kwanza na kumbeza wa pili. Hamwezi kuwatumikia wote wawili, Mungu na Mali za Nchini (Mamona). Kwa hiyo nawaambiani: Msiyasumbukie maisha yenu mkisema: Tutakula nini? Tutakunywa nini? Wala msiisumbukie miili yenu mkisema: Tutavaa nini? Je? Maisha hayapiti vyakula? Nao mwili haupiti mavazi? Watazameni ndege wa angani! Hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi waweke vichanjani. Naye Baba yenu wa mbinguni anawalisha nao. Je? Nyinyi hamwapiti hao? Tena kwenu yuko nani anayeweza kwa kusumbuka kwake kujiongezea miaka yake kipande kama cha mkono mmoja tu? Tena yale mavazi, mbona mnayasumbukia? Jifundisheni mnapoyatazama maua ya uwago yaliyoko porini kama yanavyokua! Hayafanyi kazi, wala hayafumi nguo. Lakini nawaambiani: Hata Salomo katika utukufu wake wote hakuvikwa kama moja lao. Basi Mungu akiyavika hivyo majani ya porini yanayokaa leo tu, kesho yatupwe katika mabiwi, yateketee, Je? Hatazidi kuwavika ninyi? Mbona mna mtegemea kidogo tu? Basi msisumbuke mkisema: Tutakula nini? au: Tutakunywa nini? au: Tutavaa nini? Kwani wamizimu ndio wanaoyatafuta hayo yote; lakini Baba yenu wa mbinguni amewajua, ya kuwa mnapaswa nayo hayo yote. Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na wongofu wake! Ndivyo, mtakavyopewa hayo yote. Basi, msisumbukie ya kesho! Kwani siku ya kesho itayasumbukia yaliyo yake. Inatosha, kila siku iwe na uovu wake. Msiumbue mtu, msije mkaumbuliwa! Kwani kama mnavyowaumbua wengine, ndivyo, mtakavyoumbuliwa wenyewe. Kipimo, mnachopimia wengine, ndicho, mtakachopimiwa nanyi. Nawe unakitazamiani kibanzi kilichomo jichoni mwa ndugu yako, lakini gogo lililomo jichoni mwako wewe hulioni? Au utamwambiaje ndugu yako: Ngoja, nikitoe kibanzi katika jicho lako, wewe mwenyewe ukiwa unalo gogo zima jichoni mwako? Mjanja, kwanza litoe gogo katika jicho lako! Kisha utazame vema, ndivyo upate kukitoa kibanzi katika jicho la ndugu yako! Kilichotakata msiwape mbwa, wala msiwatupie nguruwe ushanga wenu wa lulu, wasije wakaukanyaga kwa miguu yao na kuwageukia na kuwararua ninyi. Ombeni! ndipo, mtakapopewa. Tafuteni! ndipo, mtakapoona. Pigeni hodi! ndipo, mtakapofunguliwa mlango. Kwani kila anayeomba hupewa, naye anayetafuta huona, naye anayepiga hodi hufunguliwa mlango. Au kwenu yuko mtu, mwanawe anapomwomba mkate, ampe jiwe? Au anapomwomba samaki, ampe nyoka? Basi, ninyi mlio wabaya mkijua kuwapa watoto wenu vipaji vyema, Baba yenu alioko mbinguni asizidi kuwapa mema wanaomwomba? Yo yote, mnayotaka, watu wawafanyie ninyi, nanyi mwafanyie yaleyale! Kwani hayo ndiyo Maonyo na Wafumbuaji. *Uingieni mlango ulio mfinyu! Kwani liko lango lililo pana, nayo njia yake ni kubwa; ndiyo inayokwenda penye kuangamizwa, nao wanaoingia mle ni wengi. Tena uko mlango ulio mfinyu, nayo njia yake inasonga; ndiyo inayokwenda penye uzima, lakini wanaoiona ni wachache. Jilindeni kwa ajili ya wafumbuaji wa uwongo! Wanawajia wamevaa kama kondoo, lakini mioyoni ni mbwa wa mwitu wenye ukali. Kwa matunda yao mtawatambua. Je? Huchuma zabibu miibani? Au huchuma kuyu mikongeni? Hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; lakini mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu hauwezi kuzaa matunda mazuri Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa, utupwe motoni. Kwa hiyo mtawatambua kwa matunda yao. Miongoni mwao wanaoniita: Bwana! Bwana! sio wote wakaoingia katika ufalme wa mbingu, ni wao tu wanaoyafanyiza, Baba yangu alioko mbinguni ayatakayo. Siku ile wengi wataniuliza: Bwana, sisi hatukufumbua kwa Jina lako? Hatukufukuza pepo kwa Jina lako? Hatukufanya mengi yenye nguvu kwa Jina lako? Ndipo, nitakapowaambia waziwazi: Sijawatambua ninyi kabisa. Ondokeni kwangu, mliofanya maovu!* *Basi, kila mtu anayeyasikia haya maneno yangu na kuyafanyiza atafanana na mtu mwenye akili aliyeijenga nyumba yake mwambani. Mvua kubwa ikanyesha, mito ikajaa, pepo zikavuma, vyote vikaipiga ile nyumba, lakini haikuanguka, kwani misingi yake ilikuwa imejengwa mwambani. Lakini kila mtu anayeyasikia haya maneno yangu asipoyafanyiza atafanana na mtu mpumbavu aliyeijenga nyumba yake mchangani. Mvua kubwa ikanyesha, mito ikajaa, pepo zikavuma vyote vikaipiga ile nyumba, basi, ikaanguka, anguko lake likawa kubwa. Ikawa, Yesu alipokwisha kuyasema maneno haya, makundi ya watu walishangazwa na mafundisho yake. Kwani alikuwa akiwafundisha kama wenye nguvu, si kama waandishi wao.* *Alipotelemka mlimani, makundi mengi ya watu wakamfuata. Mara akaja mwenye ukoma, akamwangukia akisema: Bwana, ukitaka waweza kunitakasa. Ndipo, Yesu aliponyosha mkono, akamgusa akisema: Nataka, utakaswe. Mara ukoma ukatakaswa. Kisha Yesu akamwambia: Tazama, usimwambie mtu! Ila uende, ujionyeshe kwa mtambikaji, ukitoe kipaji, Mose alichokiagiza, kije kinishuhudie kwao. Yesu alipoingia Kapernaumu, mkubwa wa askari akamjia, akambembeleza akisema: Bwana, mtoto wangu amelala nyumbani, anaumia vibaya kwa kulemaa. Yesu akamwambia: Mimi ninakuja kumponya Lakini yule mkubwa wa askari akamjibu akisema: Bwana, hainipasi, uingie kijumbani mwangu, ila sema neno tu! ndipo, mtoto wangu atakapopona! Kwani nami ni mtu wa serikali, ninao askari chini yangu. Nami nikimwambia huyu: Nenda! basi, huenda; na mwingine: Njoo! huja; nikimwagiza mtumishi wangu: Vifanye hivi! huvifanya. Yesu alipoyasikia akastaajabu, akawaambia waliomfuata: Kweli nawaambiani: Kwa Waisiraeli sijaona bado mtu mwenye kunitegemea kama huyu. Lakini nawaambiani: Wengi watatoka maawioni na machweoni kwa jua, watakaa chakulani pamoja na Aburahamu na Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbingu, lakini wana wa huo ufalme watatupwa penye giza lililoko nje; ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno. Kisha Yesu akamwambia mkubwa wa askari: Nenda kwenu, na uyapate uliyoyategemea! Saa ileile mtoto wake akapona.* Ikawa, Yesu alipoingia nyumbani mwa Petero, akamwona mama ya mkewe Petero, amelala kwa kuwa na homa. Alipomgusa mkono, homa ikamwacha, akainuka, akamtumikia. Ilipokuwa jioni, wakampelekea wengi waliopagawa na pepo; naye akawafukuza pepo kwa neno tu. Nao wote waliokuwa hawawezi akawaponya, kusudi litimizwe lililosemwa na mfumbuaji Yesaya: Yeye ameyachukua manyonge yetu, akajitwisha maumivu yetu. Lakini Yesu alipoona, watu wengi wakimzunguka, akaagiza, wavuke kwenda ng'ambo. Ndipo, mwandishi mmoja alipomjia, akamwambia: Mfunzi, nitakufuata po pote, utakapokwenda. Yesu akamwambia: Mbweha wanayo mapango, nao ndege wa angani wanavyo vituo, lakini Mwana wa mtu hana pa kukilazia kichwa chake. Mwanafunzi wake mwingine akamwambia: Bwana, nipe ruhusa, kwanza niende, nimzike baba yangu! Yesu akamwambia: Nifuata mimi, waache wafu, wazikane wao kwa wao! *Alipoingia chomboni, wanafunzi wake wakafuatana naye. Mara kukawa na msukosuko mkubwa baharini, hata chombo kilifunikizwa na mawimbi, lakini yeye alikuwa amelala usingizi. Ndipo, walipomjia, wakamwamsha wakisema: Bwana, tuokoe, tunaangamia! Yesu akawaambia: Mbona mnaogopa hivyo? Mbona mnanitegemea kidogo tu? Kisha akainuka, akaukaripia upepo na bahari, kukawa kimya kabisa. Lakini watu wakastaajabu wakisema: Ni mtu gani huyu, ya kuwa hata upepo na bahari zinamtii?* Alipofika ng'ambo katika nchi ya Wagadara, watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitoka penye makaburi, ni wakorofi mno; kwa hiyo mtu hakuweza kuipita njia ile. Mara wakapiga kelele wakisema: Tuko na jambo gani sisi na wewe, mwana wa Mungu? Umejia hapa kutuumiza, siku zetu zikiwa hazijatimia bado? Mbali yao kulikuwako kundi la nguruwe wengi waliokuwako malishoni. Wale pepo wakambembeleza wakisema: Ukitufukuza, tutume, tuliingie lile kundi la nguruwe! Yesu alipowaambia: Haya! Nendeni! ndipo, pepo walipowatoka, wakawaingia nguruwe. Mara kundi lote likatelemka mbio mwambani, wakaingia baharini, wakafa majini; lakini wachungaji wakakimbia, wakaenda zao mjini, wakayatangaza yote, hata mambo ya wenye pepo. Mara watu wa mji wakatoka wote, wakutane na Yesu. Walipomwona wakambembeleza, atoke mipakani kwao. *Akaingia chomboni, akavuka, akafika mjini mwake yeye. Papo hapo wakamletea mgonjwa wa kupooza aliyelala kitandani. Yesu alipoona, walivyomtegemea, akamwambia mwenye kupooza: Tulia, mwanangu! Makosa yako yameondolea. Ndipo, waandishi waliokuwako waliposema mioyoni: Huyu anambeza Mungu. Kwa kuyajua hayo mawazo yao Yesu akasema: Mbona mnawaza mabaya mioyoni mwenu? Kwani kilicho chepesi ni kipi? kusema: Makosa yako yameondolewa! au kusema: Inuka, uende? Lakini kusudi mpate kujua, ya kuwa Mwana wa mtu ana nguvu ya kuondoa makosa nchini, - basi, akamwambia mwenye kupooza: Inuka, jitwishe kitanda chako, uende nyumbani kwako! Ndipo, alipoinuka akaenda nyumbani kwake. Lakini makundi ya watu walipoyaona wakaogopa, wakamtukuza Mungu aliyewapa watu nguvu kama hizo.* *Yesu alipotoka huko, aende zake, akaona mtu anayeitwa Mateo, amekaa forodhani. Akamwambia: Nifuata! Akainuka, akamfuata. Ikawa, alipokaa chakulani nyumbani mwake, ndipo, walipokuja watoza kodi na wakosaji wengi, wakakaa chakulani pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafariseo walipowaona wakawaambia wanafunzi wake: Kwa nini mfunzi wenu anakula pamoja na watoza kodi na wakosaji? Yesu alipoyasikia akasema: walio wazima hawapaswi na mganga, ila walio wagonjwa. Lakini nendeni zenu, mkajifunze maana ya neno hili: Huruma ndizo, nizitakazo, lakini vipaji vya tambiko sivyo. Kwani sikujia kuwaita wongofu, ila wakosaji.* Ndipo, walipomjia wanafunzi wa Yohana wakisema: Kwa nini sisi na Mafariseo hufunga, lakini wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia: Walioalikwa arusini hawawezi kusikitika hapo, bwana arusi akingali pamoja nao. Lakini siku zitakuja, watakapoondolewa bwana arusi; ndipo, watakapofunga. Hakuna mtu anayetia kiraka cha nguo mpya katika kanzu chakavu, kwani kinaondoa pote paliposhonwa katika kanzu, hivyo tundu lake litakuwa kubwa zaidi. Wala watu hawatii mvinyo mpya katika viriba vichakavu; kwani wakiitia mle, viriba vitapasuka, mvinyo imwagike, navyo viriba vitaangamia. Ila hutia mvinyo mpya katika viriba vipya; hivyo vyote viwili vitakaa. *Alipokuwa akiwaambia haya, mara akaja jumbe, akamwangukia akisema: Binti yangu amekufa sasa hivi; lakini uje umbandikie mkono wako! mdipo atakapokuwa mzima tena. Yesu akaondoka, akafuatana naye pamoja na wanafunzi wake. Mara akaja mwanamke mwenye kutoka damu miaka 12, akamjia nyuma, akaligusa pindo la nguo yake, maana alisema moyoni: Hata nikiigusa nguo yake tu nitapona. Lakini Yesu akageuka, akamwona, akasema: Tulia, mwanangu! Kunitegemea kwako kumekuponya. Yule mwanamke akapona saa ileile. Yesu alipoingia nyumbani mwa jumbe akawaona wapiga filimbi na kundi la watu, wakiomboleza, akasema: Ondokeni! Kwani kijana hakufa, ila amelala usingizi tu; ndipo, walipomcheka sana. Lakini wale watu walipokwisha fukuzwa, akaingia, akamshika mkono wake; ndipo, yule kijana alipoinuka. Habari hizi zikatoka, zikaenea katika nchi ile yote.* Yesu alipotoka huko, aende zake, wakamfuata vipofu wawili, wakapaza sauti za kuita: Tuhurumie, mwana wa Dawidi! Alipoingia nyumbani, wale vipofu wakamjia. Yesu akawauliza: Mwanitegemea kwamba: Naweza kufanya hivyo? Wakamwambia: Ndio, Bwana. Ndipo, alipowagusa macho akisema: Hayo, mliyoyategemea, na myapate vivyo hivyo! Ndipo, macho yao yalipofumbuka. Kisha Yesu akawakemea akisema: Angalieni, mtu hata mmoja asiyasikie haya! Lakini wale walipotoka wakamsimulia po pote katika nchi ile yote. Hao walipotoka, mara wakamletea bubu aliyepagawa na pepo. Naye pepo alipokwisha fukuzwa, yule bubu akaweza kusema. Makundi ya watu wakastaajabu wakisema: Tangu zamani havijaonekana katika Isiraeli vilivyo kama hivi. Lakini Mafariseo wakasema: Nguvu ya mkuu wa pepo ndiyo, huyu anayofukuzia pepo. *Yesu akawa akizunguka mijini mote na vijijini, akawafundisha katika nyumba zao za kuombea, akautangaza Utume mwema wa ufalme, akaponya ugonjwa wote na unyonge wote. Lakini alipowatazama makundi ya watu akawaonea uchungu, kwani walikuwa wamechoka kwa kuteswa na kutawanyishwa kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo, alipowaambia wanafunzi wake: Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Mwombeni mwenye mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake!* Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa nguvu za kufukuza pepo wachafu na za kuponya wagonjwa wo wote na wanyonge wo wote. Majina yao wale mitume kumi na wawili ndiyo haya: Wa kwanza Simoni anayeitwa Petero na Anderea nduguye, Yakobo wa Zebedeo na Yohana nduguye, Filipo na Bartolomeo, Toma na Mateo, mtoza kodi, Yakobo wa Alfeo na Tadeo, Simoni wa Kana na Yuda Iskariota aliye mchongea halafu. Hao kumi na wawili Yesu aliwatuma na kuwaagiza akisema: Msiende katika njia za wamizimu, wala mji wowote wa Wasamaria msiuingie! Lakini mwende kwa kondoo waliopotea wa mlango wa Isiraeli! Tena mnapokwenda pigeni mbiu mkisema: Ufalme wa mbingu umekaribia! Walio wagonjwa waponyeni, waliokufa wafufueni, wenye ukoma watakaseni, nazo pepo zifukuzeni! Bure mmeyapata, tena yatoeni bure! Msichukue mishipini mwenu dhahabu wala shilingi wala senti! Msichukue mkoba wa njiani wala nguo mbili wala viatu wala fimbo! Kwani mtenda kazi hupaswa na kupewa chakula chake. Lakini mji au kijiji mtakamoingia ulizeni, kama yumo mtu anayepaswa na kuwapokea! Kaeni mwake, mpaka mtakapotoka tena! Tena mkiingia nyumbani wapeni salamu! Ikiwa wamepaswa nao, utengemano wenu utakaa humo. Lakini ikiwa hawakupaswa nao, utengemano wenu utawarudia ninyi. Tena mtu asipowapokea wala asipoyasikia maneno yenu, basi, kama ni nyumba au mji, mtokeni na kuyakung'uta mavumbi ya miguuni penu! Kweli nawaambiani: Siku ya hukumu nchi ya Sodomu na Gomora itapata mepesi kuliko mji ule. Tazameni, mimi nawatuma, mwe kama kondoo walio katikati ya mbwa wa mwitu. Kwa hiyo mwe wenye mizungu kama nyoka, tena mwe wakweli, kama njiwa walivyo! Jilindeni kwa ajili ya watu! Kwani watawapeleka barazani kwao wakuu na kuwapiga katika nyumba zao za kuombea. Kwa ajili yangu watawavuta kwa mabwana wakubwa na kwa wafalme, mje mnishuhudie kwao na kwa wamizimu. Lakini hapo watakapowatoa, msihangaikie wala mizungu wala maneno ya kuwajibu! Kwani saa ileile mtapewa maneno, mtakayoyasema. Kwani si ninyi mnaosema, ila ni Roho wa Baba yenu; ndiye anayesema vinywani mwenu. Ndugu na ndugu watatoana, wauawe, hata baba watawatoa watoto wao, hata watoto watawainukia wazazi wao, wawaue. Nanyi mtakuwa mmechukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza mjini humu kimbilieni mwingine! Kwani nawaambiani iliyo kweli: Hamtaimaliza miji ya Isiraeli, mpaka Mwana wa mtu atakapokuja. *Mwanafunzi hampiti Mfunzi wake, wala mtumwa hampiti bwana wake. Inamtosha mwanafunzi kuwa, kama mfunzi wake alivyo, vilevile mtumwa inamtosha kuwa, kama bwana wake alivyo. Kama Mwenye nyumba walimwita Belzebuli (Mkuu wa pepo), hawatazidi kuwaita hivyo waliomo nyumbani mwake? Msiwaogope! Kwani hakuna lililofunikwa lisilofunuliwa halafu, wala hakuna lililofichwa lisilotambulikana halafu. Ninalowaambia gizani lisemeni mwangani! Tena ninalowanong'oneza masikioni, litangazeni barazani! Tena msiwaogope wanaoweza kuiua miili tu, wasiweze kuziua nazo roho! Lakini mfulize kumwogopa anayeweza kuziangamiza roho pamoja na miili shimoni mwa moto! Je? Videge viwili haviuzwi kwa senti moja? Lakini hata mmoja wao haanguki chini, Baba yenu asipojua. Lakini kwenu ninyi hata nywele za vichwani zimehesabiwa zote. Kwa hiyo msiogope ninyi mnapita videge vingi! Kila atakayeungama mbele ya watu, kwamba ni mtu wangu, nami nitaungama mbele ya Baba yangu wa mbinguni, kwamba ni mtu wangu. Lakini atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu wa mbinguni.* Msidhani, ya kuwa nimejia kuiletea nchi utengemano! Sikujia kuleta utengemano, ila upanga. Kwani nimejia kutenga watu, wagombane mtu na baba yake, mwana wa kike na mama yake, vilevile mkwe na mkwewe, nao watakaomchukia mtu ndio waliomo mwake. Anayempenda baba yake au mama yake kuliko mimi hanipasi; anayempenda mwanawe wa kiume au wa kike kuliko mimi hanipasi. Tena asiyejitwisha msalaba wake na kunifuata nyuma yangu hanipasi. Mwenye kuiponya roho yake ataiangamiza; mwenye kuiangamiza roho yake kwa ajili yangu ataiponya. Anayewapokea ninyi hunipokea mimi; naye anayenipokea mimi humpokea aliyenituma. Anayepokea mfumbuaji, kwa kuwa ni mfumbuaji, atapata mshahara kama wa mfumbuaji; naye anayepokea mwongofu, kwa kuwa ni mwongofu, atapata mshahara kama wa mwongofu. Tena mtu akinywesha mmoja wao walio wadogo kinyweo cha maji mazizima tu, kwa kuwa ni mwanafunzi, kweli nawaambiani: Mshahara wake hautampotea kamwe. Yesu alipokwisha kuwaagiza haya wanafunzi wake kumi na wawili akaondoka, alikokuwa, akaenda kufundisha watu na kuwapigia ile mbiu katika miji yao. *Lakini Yohana alipozisikia mle kifungoni kazi zake Kristo akatuma wanafunzi wake wawili, akamwuliza: Wewe ndiwe mwenye kuja, au tungoje mwingine? Yesu akajibu akiwaambia: Rudini, mmsimulie Yohana, mliyoyasikia nayo mliyoyaona: vipofu wanaona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanapigiwa mbiu njema. Tena mwenye shangwe ndiye asiyejikwaa kwangu. Wao walipokwenda zao, Yesu akaanza kusema na yale makundi ya watu mambo ya Yohana: Mlipotoka kwenda nyikani mlikwenda kutazama nini? Mlikwenda kutazama utete unaotikiswa na upepo? Au mlitoka kutazama nini? Mlikwenda kutazama mtu aliyevaa mavazi mororo? Tazameni, wanaovaa mavazi mororo wamo nyumbani mwa wafalme. Au mlitoka kutazama nini? Mlitaka kuona mfumbuaji? Kweli, nawaambiani: Ni mkuu kuliko mfumbuaji. Huyo ndiye aliyeandikiwa: Utaniona mimi, nikimtuma mjumbe wangu, akutangulie, aitengeneze njia yako mbele yako.* Kweli nawaambiani: Miongoni mwao wote walizaliwa na wanawake hajaonekana aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji. Lakini aliye mdogo katika ufalme wa mbingu ni mkuu kuliko yeye. Tangu siku za Yohana Mbatizaji mpaka leo ufalme wa mbingu huendewa kwa nguvu, nao wenye nguvu lhuupoka. Kwani Wafuambuaji wote nayo Maonyo waliufumbua, mpaka Yohana akitokea. Tena kama mnataka kuitikia: Yeye ndiye Elia atakayekuja. Mwenye masikio yanayosikia na asikie! *Lakini wao wa kizazi hiki niwafananishe na nini? Wamefanana na watoto wanaokaa sokoni na kuwaita wenzi wao wakisema: Tumewapigia filimbi, nanyi hamkucheza; tena tumewaombelezea, nanyi hamkulia. Kwani Yohana alikuja, hakula, wala hakunywaakala, wakasema: Ana pepo. Mwana wa mtu alikuja, akala, akanywa, wakasema: Tazameni mtu huyu mlaji na mnyuwaji wa mvinyo, mpenda watoza kodi na wakosaji! Lakini werevu hutokezwa na matendo yake kuwa wa kweli. Ndipo Yesu alipoanza kuikaripia miji, yalimofanyika ya nguvu yake mengi, kwa maana haikujuta. Akasema: Yatakupata, wewe Korasini! Yatakupata, wewe Beti-Saida! Kwani ya nguvu yaliyofanyika kwenu, kama yangalifanyika Tiro na Sidoni, wangalijuta kale na kujivika magunia na kujikalisha majivuni. Lakini nawaambiani: Siku ya hukumu miji ya Tiro na Sidoni itapata machungu yaliyo madogo kuliko yenu. Nawe Kapernaumu, hukupazwa mpaka mbinguni? Utatumbukia mpaka kuzimuni, kwani ya nguvu yaliyofanyika kwako, kama yangalifanyika Sodomu, ungalikuwako mpaka leo. Lakini nawaambiani: Siku ile ya hukumu nchi ya Sodomu itapata machungu yaliyo madogo kuliko yako.* *Siku zile Yesu akasema kwamba: Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwani hayo umewaficha werevu na watambuzi, ukawafunulia wachanga. Ndio, Baba, kwani hivyo ndivyo, ulivyopendezwa navyo. Vyote nimepewa na Baba yangu. Hakuna anayemtambua Mwana pasipo Baba; wala hakuna anayemtambua Baba pasipo mwana na kila, Mwana atakayemfunulia. Njoni kwangu nyote, wenye kusumbuka na wenye kulemewa na mizigo! Mimi nitawatuliza. Twaeni kata yangu, mjifunze kwangu! Kwani ndimi mpole na mnyenyekevu moyoni. Kwa hivyo mtaipatia mioyo yenu kituo; kwani kata yangu ni njema, nao mzigo wangu ni mwepesi.* Siku zile Yesu alipita katika mashamba siku ya mapumziko; nao wanafunzi wake walipoona njaa wakaanza kukonyoa masuke, wakala. Lakini Mafariseo walipoviona wakamwambia: Tazama, wanafunzi wako wanafanya yaliyo mwiko kuyafanya siku ya mapumziko. Naye akawaambia: Hamkusoma, Dawidi alivyofanya alipoona njaa yeye na wenziwe? Hapo aliingia Nyumbani mwa Mungu, wakaila mikate aliyowekewa Bwana, nayo kuila ni mwiko kwake na kwa wenziwe, huliwa na watambikaji peke yao. Tena hamkusoma katika Maonyo, ya kuwa siku za mapumziko watambikaji wa pale Patakatifu huivunja miiko ya siku ya mapumziko, nao hawakosi? Lakini nawaambiani: Hapa yupo aliye mkuu kuliko Patakatifu. Lakini kama mngalitambua maana ya neno la kwamba: Huruma ndizo, nizitakazo, lakini vipaji vya tambiko sivyo, basi, hamngaliwawazia mabaya wasio na kosa. Kwani Mwana wa mtu ni bwana wa siku ya mapumziko.* Alipoondoka huko akaenda kuingia katika nyumba yao ya kuombea. Akaona mtu mwenye mkono uliokaukiana. Wakamwuliza wakisema: Iko ruhusa kuponya siku ya mapumziko? maana walitafuta la kumsuta. Nay akawaambia: Mwenye kondoo mmoja tu akitumbukiwa naye shimoni siku ya mapumziko, kwenu yuko asiyemkamata na kumwopoa? Je? Mtu hapiti kondoo kabisa? Kwa hiyo iko ruhusa kufanya mema siku ya mapumziko. Ndipo, alipomwambia yule mtu: Unyoshe mkono wako! Nao, alipounyosha, ukageuka kuwa mzima kama ule mwingine. Lakini Mafariseo wakatoka, wakamlia njama ya kumwangamiza. Yesu alipoyatambua akaondoka kule. Watu wengi wakamfuata, akawaponya wote; lakini akawatisha, wasimtangaze, kusudi litimie, mfumbuaji Yesaya alilolisema: Tazameni, huyu ndiye mtoto wangu, niliyemchagua; ni mpendwa wangu, ambaye Roho yangu inapendezwa naye. Nitamtia Roho yangu, awatangazie wamizimu, ya kwamba hukumu yao iko. Hatateta, wala hatapiga kelele, wala mtu hatamsikia kinywa chake majiani. Utete uliopondeka hatauvunja kabisa, wala utambi unaotoka moshi bado hatauzima, mpaka aitokeze ile hukumu kuwa ya kushinda. Jina lake ndilo, wamizimu watakalolingojea. Hapo akaletewa mwenye pepo aliyekuwa kipofu na bubu. Alipomponya, yule bubu akapata kusema na kuona. Ndipo, makundi ya watu waliposhangaa wote wakisema: Kumbe huyu siye mwana wa Dawidi? Mafariseo walipoyasikia wakasema: Huyu hafukuzi pepo, isipokuwa kwa nguvu ya Belzebuli aliye mkuu wa pepo. Kwa kuyajua hayo mawazo yao, Yesu akawaambia: Kila ufalme unapogombana wao kwa wao huwa mahame tu, nao kila mji au nyumba tu inapogombana wao kwa wao haitasimamika. Naye Satani akimfukuza Satani mwenziwe amejigombanisha mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamikaje? Nami nikiwafukuza pepo kwa nguvu ya Belzebuli, Je? Wana wenu huwafukuza kwa nguvu ya nani? Kwa hiyo hao ndio watakaowaumbua. Lakini mimi nikiwafukuza pepo kwa nguvu ya Roho ya Mungu, ufalme wa Mungu umekwisha kuwafikia ninyi. Au mtu atawezaje kuingia katika nyumba ya mwenye nguvu, aviteke vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Kisha ataweza kuiteka nyumba yake. Asiye wa upande wangu hunikataa; naye asiyekusanya pamoja nami hutapanya. Kwa hiyo nawaambiani: Kila kosa na kila neno la kumbeza Mungu watu wataondolewa, lakini la kumbeza Roho hawataondolewa. Mtu ye yote atakayesema neno la kumkataa Mwana wa mtu ataondolewa; lakini mtu atakayesema neno la kumkataa Roho Mtakatifu hataondolewa, wala katika ulimwengu huu wa sasa, wala katika ule utakaokuja. Mkipanda mti nzuri, basi mtapata hata matunda mazuri. Au mkipanda mti mwovu, basi, mtapata hata matunda maovu. Kwani mti hutambulikana kwa matunda yake. Enyi wana wa nyoka, mnawezaje kusema mema, mlio wabaya? Kwani moyo unayoyajaa, ndiyo, kinywa kinayoyasema. Mtu mwema hutoa mema katika kilimbiko chake chema, lakini mtu mbaya hutoa mabaya katika kilimbiko chake kibaya. Nami nawaambiani: Siku ya hukumu watu wataulizwa kila neno baya walilolisema. Kwani kwa maneno yako utapata wongofu, vile vile utapata hukumu kwa maneno yako. Hapo walikuwapo waandishi na Mafariseo, wakamwuliza wakisema: Mfunzi, twataka, ufanye kielekezo, tukione. Naye akajibu akiwaambia: Wao wa ukoo huu mbaya wenye ugoni wanatafuta kielekezo, lakini hawatapata kielekezo, ila kielekezo cha mfumbuaji Yona. Kwani kama Yona alivyokuwa tumboni mwa nyangumi siku tatu mchana na usiku, vivyo naye Mwana wa mtu atakuwa ndani ya nchi siku tatu mchana na usiku. Siku ya hukumu waume wa Niniwe watauinukia ukoo huu, wauumbue; kwani walijuta kwa tangazo la Yona. Tena tazameni, hapa yupo anayempita Yona! Yule mfalme wa kike aliyetoka kusini atauinukia ukoo huu siku ya hukumu auumbue. Kwani yeye alitoka mapeoni kwa nchi, aje kuusikia werevu wa Salomo uliokuwa wa kweli. Tena tazameni, hapa yupo anayempita Salomo! Pepo mchafu anapomtoka mtu hupita mahali pasipo na maji akitafuta kituo asikione. Halafu husema: Nitarudi nyumbani mwangu, nilimotoka. Anapokuja huiona, ni tupu, tena imefagiwa na kupambwa; ndipo, anapokwenda kuchukua pepo saba wengine walio wabaya kuliko yeye, wawe wenziwe; nao huingia, wakae humo: hivyo ya mwisho ya mtu yule yatakuwa mabaya kuliko ya kwanza. Ndivyo, vitakavyowapata wao wa ukoo huu ulio mbaya. *Alipokuwa akisema bado na makundi ya watu, mara mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje kwa kumtaka, waseme naye. Mtu akamwambia: Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje kwa kutaka, waseme na wewe. Naye akajibu akimwambia yule aliyesema naye: Mama yangu ni nani? Nao ndugu zangu ni akina nani? Akawanyoshea wanafunzi wake mkono, akasema: Watazameni walio mama yangu na ndugu zangu! Kwani mtu ye yote atakayeyafanya, ayatakayo Baba yangu alioko mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu na dada yangu na mama yangu.* Siku ile Yesu alitoka nyumbani, akaenda kukaa kandokando ya bahari. Wakamkutanyikia makundi mengi ya watu, kwa hiyo akaingia chomboni, akakaa humo, watu wote wakisimama pwani. Akawaambia maneno mengi kwa mifano akisema: Tazameni, mpanzi alitoka kumiaga mbegu. Ikawa alipozimiaga, nyingine zikaangukia njiani; ndege wakaja, wakazila. Nyingine zikaangukia penye miamba pasipo na udongo mwingi. Kuota zikaota upesi kwa kuwa na udongo kidogo; lakini jua lilipokuwa kali, zikanyauka, kwa kuwa hazina mizizi. Nyingine zikaangukia penye miiba; nayo miiba ilipoota ikazisonga. Lakini nyingine zikaangukia penye mchanga mzuri, zikazaa, nyingine punje mia, nyingine sitini, nyingine thelathini. Mwenye masikio yanayosikia na asikie! Wanafunzi wake wakamjia, wakamwambia: Sababu gani unasema nao kwa mifano? Naye akajibu akisema: Ninyi mmepewa kuyatambua mafumbo ya ufalme wa mbingu, lakini wale hawakupewa. Kwani ye yote aliye na mali atapewa, ziwe nyingi zaidi; lakini asiye na kitu atachukuliwa hata kile, alicho nacho. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano, kwamba wakitazama wasione, wakisikiliza wasisikie na kujua maana. Hivyo ufumbuo wa Yesaya unatimizwa kwao unaosema: Kusikia mtasikia, lakini hamtajua maana; kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Kwani mioyo yao walio ukoo huu imeshupazwa, hata kwa masikio yao yaliyo mazito hawasikii; nayo macho yao wameyasinziza, wasije wakaona kwa macho, au wakasikia kwa masikio, au wakajua maana kwa mioyo, wakanigeukia, nikawaponya. Lakini yenye shangwe ni macho yenu, kwani huona, nayo masikio yenu, kwani husikia. Kweli nawaambiani: Wengi waliokuwa wafumbuaji na waongofu waliyatunukia, wayaone, mnayoyaona ninyi, lakini hawakuyaona; waliyatunukia wayasikie, mnayoyasikia ninyi, lakini hawakuyasikia. Basi, ninyi usikieni mfano wa mpanzi! Kila anayelisikia Neno la ufalme asipolijua maana, huja yule Mbaya na kulinyakua lililomiagwa moyoni mwake. Hizo ndizo zilizomiagwa njiani. Lakini zilizomiagwa penye miamba ni kama mtu anayelisikia Neno na kulipokea papo hapo kwa furaha. Lakini hana mizizi moyoni mwake, ila analishika kwa kitambo kidogo tu. Yanapotukia maumivu au mafukuzo kwa ajili ya Neno, mara hujikwaa. Lakini zilizomiagwa penye miiba ni kama mtu anayelisikia Neno, lakini masumbuko ya dunia hii na udanganyifu wa mali hulisonga Neno, lisizae matunda. Lakini zilizomiagwa penye mchanga mzuri ni kama mtu anayelisikia Neno na kulijua maana. Ndiye mwenye kuzaa, mwingine huleta punje mia, mwingine sitini, mwingine thelathini. *Akawatolea mfano mwingine akisema: Ufalme wa mbingu umefanana na mtu aliyemiaga mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini watu walipolala, akaja mchukivu wake, akamiaga mbegu za nyasi katikati ya ngano, akaenda zake. Halafu majani ya ngano yalipoota na kuchanua, zikaonekana nazo nyasi. Watumwa wa mwenye shamba wakaja wakamwuliza: Bwana, hukumiaga mbegu nzuri katika shamba lako? Basi, nyasi limezipata wapi? Alipowaambia: Mtu aliye mchukivu amevifanya hivyo, watumwa wakamwambia: Unataka, twende, tuzing'oe na kuzikusanya? Akasema: Hapana, msije, mkazing'oa nazo ngano mkiwa mnakusanya nyasi. Acheni, zikue zote mbili pamoja, mpaka mavuno yatakapokuwa! Siku za kuvuna nitawaambia wavunaji: Kusanyeni kwanza nyasi, mzifunge matitatita, mziteketeze! Lakini ngano zitieni chanjani kwangu!* *Akawatolea mfano mwingine akisema: Ufalme wa mbingu umefanana na kipunje cha haradali, alichokitwaa mtu na kukipanda katika shamba lake. Nacho ni kidogo kuliko mbegu zote. Lakini kinapokua ni mkubwa kuliko miboga yote inayopandwa, huwa mti mzima, hata ndege wa angani huja na kutua katika matawi yake. Akawaambia mfano mwingine: Ufalme wa mbingu umefanana na chachu, mwanamke akiitwaa akaichanganya na pishi tatu za unga, mpaka ukachachwa wote. Haya yote aliwaambia makundi ya watu kwa mifano, pasipo mfano hakuwaambia neno, kusudi litimie lililosemwa na mfumbuaji, akisema: Nitakifumbua kinywa changu, kiseme mifano. Nitatangaza mambo yaliyofichika tangu hapo, ulimwengu ulipoumbwa.* Kisha Yesu akawaaga makundi ya watu, akaingia nyumbani. Ndipo, wanafunzi wake walipomjia wakisema: Tuelezee mfano wa nyasi za shambani! Akajibu akisema: Mwenye kumiaga mbegu nzuri ni Mwana wa mtu. Nalo shamba ndio ulimwengu. Nazo mbegu nzuri ndio wana wa ufalme. Lakini nyasi ndio wana wa yule Mbaya. Naye mchukivu aliyezimiaga ndiye Msengenyaji. Nayo mavuno ndio mwisho wa dunia. Nao wavunaji ndio malaika. Kama nyasi zinavyokusanywa na kuteketezwa motoni, ndivyo, itakavyokuwa katika mwisho wa dunia hii: Mwana wa mtu atawatuma malaika zake, nao watakusanya na kuyatoa katika ufalme wake makwazo yote nao waliofanya maovu, wawatupe shimoni mwa moto; ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno. Ndipo, waongofu watakapoangaza kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio yanayosikia na asikie! *Ufalme wa mbingu umefanana na fedha zilizofukiwa shambani. Mtu alipoziona akazifukia, akaenda kwa furaha yake, akaviuza vyote, alivyokuwa navyo, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbingu umefanana na mchuuzi aliyetafuta ushanga wa lulu nzuri. Naye alipoona lulu moja yenye bei kubwa akaenda, akaviuza vyote alivyokuwa navyo, akainunua.* Tena ufalme wa mbingu umefanana na wavu uliotupwa baharini, ukakusanya samaki wa kila mtindo. Hata ulipojaa, wakauvuta pwani, wakakaa, wakawachagua samaki, walio wazuri wakawaweka vyomboni, lakini walio wabaya wakawatupa. Hivyo ndivyo, itakavyokuwa katika mwisho wa dunia hii: Malaika watatokea, watawatenga wabaya kati ya waongofu, wawatupe shimoni mwa moto. Ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno. Mmeijua maana ya hayo yote? Walipomwambia: Ndio, akawaambia: Kwa sababu hii kila mwandishi aliyefundishiwa ufalme wa mbingu amefanana na mtu mwenye nyumba anayetoa mawekoni mwake mambo mapya na ya kale. Ikawa, Yesu alipokwisha kuisema mifano hiyo akatoka, akaenda zake. Alipofika kwao, alikokulia, akawafundisha katika nyumba yao ya kuombea, nao wakashangaa wakisema: Huyu amepata wapi werevu huu ulio wa kweli na nguvu hizi? Huyu si mwana wa seremala? Mama yake si yeye anayeitwa Maria? Nao ndugu zake sio akina Yakobo na Yosefu na Simoni na Yuda? Nao maumbu zake hawako wote kwetu? Basi, huyu amepata wapi haya yote? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia: Mfumbuaji habezwi, isipokuwa kwao, alikokulia, namo nyumbani mwake. Kwa hiyo hakufanya kule ya nguvu mengi, kwa sababu walikataa kumtegemea. Siku zile mfalme Herode alipousikia uvumi wa Yesu, akawaambia watoto wake: Huyo ndiye Yohana Mbatizaji, amefufuka katika wafu, kwa sababu hii nguvu hizo humtendesha kazi. Kwani Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia kifungoni kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, Filipo. Kwani Yohana alimwambia: Ni mwiko kwako kuwa naye. Naye alitaka kumwua, lakini aliwaogopa watu, kwani walimwona Yohana kuwa mfumbuaji. Ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia akacheza ngoma mbele yao, akampendeza Herode. Ndipo, alipomwapia kumpa cho chote, atakachomwomba. Naye kwa hivyo, alivyokwisha kuhimizwa na mama yake, akasema: Nipe sasa hivi katika chano kichwa chake Yohana Mbatizaji! Mfalme akasikitika, lakini kwa ajili ya viapo vyake na kwa ajili ya wale waliokaa naye chakulani akaagiza, apewe. Akatuma mtu, akamkata Yohana kichwa kifungoni. Kisha hicho kichwa chake kikaletwa katika chano, msichana akapewa, akampelekea mama yake. Kisha wanafunzi wake wakaja, wakautwaa mwili wake, wakauzika; kisha wakaenda, wakampasha Yesu habari. Yesu alipoyasikia akaingia chomboni, akaondoka huko kwenda peke yake mahali palipokuwa pasipo watu. Nayo makundi ya watu walipovisikia wakamfuata kwa miguu toka mijini. Yesu alipotoka chomboni akaona, watu ni wengi sana, akawaonea uchungu, akawaponya waliokuwa hawawezi. Ilipokuwa jioni, wanafunzi wake wakamjia, wakasema: Hapa tulipo ni nyika, nazo saa za mchana zimepita; basi, waage hawa watu wengi, waende zao vijijini, wajinunulie vyakula! Yesu akawaambia: Waendeje? Wapeni ninyi vyakula! Nao wakamwambia: Hatuna kitu hapa ila mikate mitano na visamaki viwili. Naye akasema: Nileteeni hapa! Akawaagiza hao watu wengi, wakae chini majanini. Akaitwaa ile mikate mitano na vile visamaki viwili, akatazama juu mbinguni akaviombea, akawamegea, akawapa wanafunzi ile mikate; nao wanafunzi wakawapa wale watu wengi. Wakala wote, wakashiba. Kisha wakayaokota makombo ya mikate yaliyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili. Nao waliokula walikuwa waume tu kama 5000 pasipo wanawake na watoto. Kisha Yesu akawashurutisha wanafunzi waingie chomboni, wamtangulie kwenda ng'ambo, mpaka yeye kwanza awaage makundi ya watu. Naye alipokwisha kuwaaga makundi ya watu akapanda mlimani peke yake kuomba. Jua lilipokwisha kuchwa, akawa huko peke yake. Nacho chombo kilikuwa kimeendelea kitambo kirefu kikahangaishwa na mawimbi, kwani upepo uliwatokea mbele. Ilipofika zamu ya nne ya usiku, akawajia akienda juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona, anavyokwenda juu ya bahari, wakatetemeka wakisema: ni mzimu! wakalia kwa woga. Papo hapo Yesu akawaambia akisema: Tulieni! Ni miye, msiogope! Petero akamjibu akisema: Bwana, ukiwa ni wewe, agiza nije kwako majini juujuu! Alipomwambia: Njoo! Petero akashuka chomboni, akaenda juu ya maji, amfikie Yesu. Lakini alipotazama, upepo ulivyo na nguvu, akaogopa, akaanza kuzama majini, akapiga kelele akisema: Bwana, niokoa! Mara Yesu akaunyosha mkono, akamshika, akamwambia: Mbona unanitegemea kidogo tu? Mbona umeingiwa na wasiwasi? Walipopanda chomboni, upepo ukakoma. Nao waliokuwamo chomboni wakamwangukia wakisema: Kweli ndiwe Mwana wa Mungu! Walipokwisha vuka wakafika nchini kwa Genesareti. Wenyeji wa huko walipomtambua wakatuma watu kwenda katika nchi zote za pembenipembeni, wakamletea wote waliokuwa hawawezi. Wakambembeleza, wamguse pindo la kanzu yake tu; nao wote walioligusa wakapona kabisa. Ndipo, walipomjia Yesu Mafariseo na waandishi waliotoka Yerusalemu, wakasema: Kwa sababu gani wanafunzi wako hawayafuati mazoezo ya wakale? Kwani hawanawi mikono wakila chakula. Ndipo, alipowajibu akisema: Nanyi sababu gani hamlifuati agizo lake Mungu kwa ajili ya mazoezo ya wakale wenu? Kweli Mungu alisema: Mheshimu baba yako na mama yako! na tena: Atakayemwapiza baba au mama sharti afe kwa kuuawa! Lakini ninyi husema: Mtu akimwambia baba au mama: Mali, unazozitaka, nikusaidie nazo, amepewa Mungu, basi, ni vema. Hivyo hatamheshimu baba na mama tena; ndivyo, mlivyolitangua Neno la Mungu kwa ajili ya mazoezo ya wakale wenu. Enyi wajanja, Yesaya aliwafumbua vizuri hayo mambo yenu aliposema: Ukoo huu huniheshimu kwa midomo tu, lakini mioyo yao inanikalia mbali. Hivyo hunicha bure, kwani hufundisha mafundisho yaliyto maagizo ya watu tu. Akaliita kundi la watu, akawaambia: Sikilizeni, mjue maana! Kinachoingia kinywani sicho kinachomtia mtu uchafu, ila kinachotoka kinywani ndicho kinachomtia mtu uchafu. Ndipo, wanafunzi walipomjia, wakamwuliza: Unajua, ya kuwa Mafariseo walikwazwa walipolisikia neno hilo? Naye akajibu akisema: Kila mmea, asioupanda Baba yangu wa mbinguni, utang'olewa. Waacheni hao! Ni mapofu wenye kuongoza vipofu wenzao. Kipofu akimwongoza kipofu mwenziwe, wote wawili watatumbukia shimoni. Petero akajibu, akamwambia: Tuelezee mfano huu! Naye akasema: Kumbe nanyi hajaerevuka hata leo! Hamjui, kila kitu kinachoingia kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni? Lakini yanayotoka kinywani mwa mtu yametoka moyoni mwake, nayo ndiyo yanayomtia mtu uchafu. Kwani moyoni hutoka mawazo mabaya: uuaji, uzinzi, ugoni, wizi, usingiziaji, matusi. Haya ndiyo yanayomtia mtu uchafu; lakini kula na mikono isiyonawiwa hakumtii mtu uchafu. *Yesu alipotika huko akajiepusha kwenda pande za Tiro na Sidoni. Mara mwanamke wa Kikanaani aliyekaa mipakani huko akatokea, akapaza sauti akisema: Nihurumie, Bwana, mwana wa Dawidi! Binti yangu anapagawa vibaya na pepo. Lakini hakumjibu neno. Wanafunzi wake wakamjia, wakamwomba wakisema: Mwache, aende zake! Kwani anatupigia kelele nyuma yetu. Naye akajibu: Sikutumwa pengine, ni kwao tu walio kondoo waliopotea wa mlango wa Isiraeli. Naye mwanamke akaja, akamwangukia, akasema: Bwana, nisaidie! Naye akajibu akisema: Haifai kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia vijibwa. Mwanamke akasema: Ndio Bwana, lakini nao vijibwa hula makombo yanayoanguka mezani pa bwana zao. Ndipo, Yesu alipojibu akimwambia: Mama, umenitegemea kabisa. Na uvipate unavyovitaka! Saa ile ile binti yake akapona.* Kisha Yesu akaondoka huko, akafika kandokando ya bahari ya Galilea, akapanda mlimani, akakaa huko. Wakamjia makundi mengi ya watu walio na viwete na wenye vilema na vipofu na mabubu na wengine wengi pamoja nao. Wakawaweka miguuni pa Yesu, naye akawaponya. Ikawa, makundi ya watu wakastaajabu waliupoona, mabubu wakisema, nao waliolemaa wakiwa wazima, nao viwete wakitembea, nao vipofu wakiona. Wakamtukuza Mungu wa Isiraeli. Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema: Kundi hili la watu nalionea uchungu, kwa kuwa wameshinda kwangu siku tatu, wasione chakula. Nami sitaki kuwaaga, waende zao pasipo kula, maana wasije, wakazimia njiani. Wanafunzi wakamwambia: Hapa nyikani tutapata wapi mikate inayotosha kuwashibisha watu walio wengi kama hawa? Yesu akawauliza: Mnayo mikate mingapi? Nao waliposema: Tunayo saba na visamaki vichache, akawaagiza hao watu wengi, wakae chini. Kisha akaitwaa ile mikate saba na samaki, akashukuru, akaimega akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawapa wao wa makundi ya watu. Wote wakala, wakashiba; kisha wakayaokota makombo ya mikate yaliyosalia, wakajaza makanda saba. Nao waliokula walikuwa waume tu 4000 pasipo wanawake na watoto. Kisha akawaaga makundi, waende zao, akaingia chomboni, akaja mipakani kwa Magadala. Wakaja Mafariseo na Masadukeo, wakamjaribu wakitaka, awaonyeshe kielekezo kitokacho mbinguni. Naye akajibu akiwaambia: Kukichwa mnasema: Kutakucha na kianga, kwani mbingu ni nyekundu. Tena kukicha mnasema: Leo itakunya mvua, kwani mbingu ni nyekundu, tena kumetanda mawinguwingu. Enyi wajanja! Mnayoyaona ya mbinguni, mnajua kuyatambua, lakini vielekezo vya siku hizi vinawashindani? Wao wa ukoo huu mbaya wenye ugoni wanataka kielekezo, lakini hawatapata kielekezo, ila kielekezo cha mfumbuaji Yona. Kisha akawaacha, akaenda zake.* Wanafunzi walipofika ng'ambo walikuwa wamesahau kuchukua mikate. Yesu akawaambia: Tazameni, jilindeni kwa ajili ya chachu yao Mafariseo na Msadukeo! Ndipo, walipoyafikiri na kusemeza wao kwa wao: Ni kwa sababu hatukuchukua mikate; Lakini Yesu akawatambua, akawaambia: Enyi mnaonitegemea kidogo tu, mbona mnafikiri hivyo mioyoni mwenu ya kuwa hamnayo mikate? Hamjaerevuka bado? Wala hamwikumbuki mikate ile mitano ya wale 5000 na makapu, mliyoyachukua, kama ni mangapi? Wala hamwikumbuki ile mikate saba ya wale 4000 na makanda, mliyoyachukua, kama ni mangapi? Kwa sababu gani hamtambui, ya kuwa sikuwaambia kwa ajili ya mikate niliposema: Jilindeni kwa ajili ya chachu yao Mafariseo na Masadukeo? Ndipo, walipotambua, ya kuwa hakusema, wajilinde kwa ajili ya chachu ya mikate, ila wajilinde kwa ajili ya ufundisho wao Mafariseo na Masadukeo. Yesu akaenda pande za mji wa Kesaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akisema: Watu humsema Mwana wa mtu kuwa ni nani? Nao wakajibu: Wengine husema kuwa u Yohana Mbatizaji, wengine: Elia, wengine: Yeremia au mmoja wao wafumbuaji. Yesu akawauliza: Lakini ninyi mnanisema kuwa ni nani? Simoni Petero akajibu akisema wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mungu Mwenye uzima. Yesu akajibu akimwambia: U mwenye shangwe, Simoni wa Yona, kwani mwenye mwili na damu hakukufunulia hili, ila Baba yangu alioko mbinguni. Nami nakuambia: Wewe ndiwe Petero, juu ya mwamba huu nitalijenga kundi la wateule wangu, nayo malango ya kuzimu hayatawashinda. Nitakupa funguo za ufalme wa mbingu: lo lote, utakalolifunga nchini, litakuwa limefungwa hata mbinguni; nalo lo lote, utakalolifungua nchini, litakuwa limefunguliwa hata mbinguni. Ndipo, alipowatisha wanafunzi, wasimwambie mtu ya kuwa yeye ndiye Kristo. *Tokea hapo Yesu Kristo akaanza kuwaonyesha wanafunzi wake, ya kuwa imempasa kwenda Yerusalemu ateswe mengi nao wazee na watambikaji wakuu na waandishi, mpaka auawe, kisha afufuliwe siku ya tatu. Ndipo, Petero alipomchukua pembeni, akaanza kumtisha akisema: Jionee uchungu, wewe Bwana, haya yasikupate! Naye akageuka, akamwambia Petero: Niondokea hapa nyuma yangu, wewe Satani! Wewe wataka kunikwaza, kwani wewe huyawazi mambo ya Kimungu, ila unayawaza ya kiwatu tu. Ndipo, Yesu alipowaambia wanafunzi wake: Mtu akitaka kunifuata mimi ajikataze mapenzi yake, ajitwishe nao msalaba wake, kisha anifuate! Maana mtu anayetaka kuikoa roho yake ataiangamiza. Lakini mtu atakayeiangamiza roho yake kwa ajili yangu mimi ataiponya. Kwani mtu vitamfaa nini, hata avichume vya ulimwengu wote, roho yake ikiponwa navyo? Au mtu atatoa nini, aikomboe roho yake?* Kwani Mwana wa mtu atakapokuja mwenye utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, ndipo, atakapomlipa kila mtu, kama matendo yake yalivyo. Kweli nawaambiani: Miongoni mwao wanaosimama hapa wamo wengine, ambao hawatakuonja kufa, mpaka watakapomwona Mwana wa mtu, akija mwenye ufalme wake. Baada ya siku sita Yesu akamchukua Petero na Yakobo na Yohana nduguye, akapanda pamoja nao peke yao juu ya mlima mrefu. Huko akageuzwa sura yake machoni pao. Uso wake ukamulika kama jua, nazo nguo zake zikamerimeta kama mwanga. Walipotazama, wametokewa na Mose na Elia, wanaongea na Yesu. Petero akasema akimwambia Yesu: Bwana, hapa ni pazuri kuwapo sisi. Ukitaka, nitajenga hapa vibanda vitatu; kimoja chako, na kimoja cha Mose, na kimoja cha Elia. Angali akisema, mara wingu jeupe likawatia kivuli, sauti ikatoka winguni, ikisema: Huyu ndiye mwanangu mpendwa, ambaye nimependezwa naye. Msikilizeni yeye! Wanafunzi walipoyasikia wakaanguka kifudifudi, wakaingiwa na woga sana. Yesu akawaendea, akasema akiwagusa: Inukeni, msiogope! Walipoyainua macho yao, hakuna waliyemwona, asipokuwa Yesu peke yake. Walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu akawaagiza akisema: Msimwambie mtu ye yote mliyoyaona, mpaka Mwana wa mtu atakapofufuliwa katika wafu!* Nao wanafunzi wakamwuliza wakisema: Basi, waandishi husemaje: Sharti kwanza Elia aje? Naye akajibu akisema: Kweli Elia anakuja, vyote avigeuze kuwa vipya. Lakini nawaambiani: Elia amekwisha kuja, nao hawakumtambua, wakamtendea yote, waliyoyataka. Hivyo hata Mwana wa mtu atateswa nao. Hapo ndipo wanafunzi walipojua, ya kuwa amewaambia mambo ya Yohana Mbatizaji. Walipofika penye kundi la watu, mtu akamjia, akampigia magoti, akasema: Bwana, umhurumie mwanangu! Kwani ni mwenye kifafa, aumia vibaya. Kwani mara nyingi huanguka motoni, tena mara nyingi huanguka majini. Nikampeleka kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya. Yesu akajibu akisema: Enyi wa kizazi kisichomtegemea Mungu kwa kupotoka! Nitakuwapo nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni hapa, nilipo! Yesu alipomkaripia, pepo akamtoka; naye mtoto akapona tangu saa ileile. Kisha wanafunzi wakamjia Yesu, alipokuwa peke yake, wakasema: Mbona sisi hatukuweza kumfukuza huyo? Naye akawaambia: Ni kwa ajili hammtegemei Mungu vema. Maana nawaambia la kweli: Cheo chenu cha kumtegemea Mungu kikiwa kidogo kama kipunje cha mbegu, mtauambia mlima huu: Ondoka hapa, ulipo, uende pale! nao utaondoka. Hivyo halitakuwako neno lisilowezekana nanyi. Lakini kabila hili la pepo halitoki isipokuwa kwa nguvu ya kuomba na ya kufunga. Walipokuwa wakizunguka huko Galilea, Yesu akawaambia: Mwana wa mtu atatiwa mikononi mwa watu, nao watamwua, kisha siku ya tatu atafufuliwa. Wakasikitika sana. Walipofika Kapernaumu, watoza kodi wakamjia Petero, wakasema: Mfunzi wenu halipo kodi? Akasema: Hulipa. Naye alipokuja nyumbani, Yesu akaanza kumwuliza akisema: Waonaje, Simoni, wafalme wa nchi huwatoza watu gani chango au kodi? Wana wao wenyewe au wageni? Alipojibu: Huwatoza wageni, Yesu akamwambia: Basi, wana wenyewe hawatozwi. Lakini tusiwakwaze! Nenda pwani, uloe kwa ndoana! Kisha samaki wa kwanza atakayezuka umshike, ufumbue kinywa chake! Mle utaona fedha, itwae, ukawape kwa ajili yetu, mimi na wewe! Saa ile wanafunzi wakamjia Yesu, wakamwuliza wakisema: Aliye mkuu katika ufalme wa mbingu ni nani? Akaita kitoto, akamsimamisha katikati yao, akasema: Kweli nawaambiani: Msipogeuka, mkawa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbingu. Mtu atakayejinyenyekeza mwenyewe, awe kama kitoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbingu. Naye atakayepokea kitoto mmoja kama huyu kwa jina langu hunipokea mimi. Lakini mtu atakayekwaza mmoja tu aliye mwenzao hawa wadogo wanaonitegemea inamfaa kutungikwa shingoni pake jiwe kubwa la kusagia, kisha atoswe kilindini mwa bahari. Yako yatakayoupata ulimwengu kwa ajili ya makwazo. Kweli makwazo sharti yaje, lakini mtu yule anayelileta kwazo atapatwa na mambo. Nawe, mkono wako ukikukwaza, au mguu wako ukikukwaza, uukate uutupe mbali! Kuingia penye uzima mwenye kilema au kiwete kutakufaa kuliko hapo, ukiwa mwenye mikono miwili au miguu miwili, ukatupwa katika moto usiozimika kale na kale. Nalo jicho lako likikukwaza, basi ling'oe ulitupe mbali! Kuingia penye uzima mwenye chongo kutakufaa kuliko hapo, ukiwa mwenye macho mawili, ukatupwa shimoni mwa moto. Tazameni, msiwabeze wadogo hawa hata mwenzao mmoja! Kwani nawaambiani: Malaika zao mbinguni huutazama siku zote uso wa Baba yangu alioko mbinguni. Kwani Mwana wa mtu amekuja kukiokoa kilichoangamia. Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, tena mmoja wao akipotea, hatawaacha wale tisini na tisa milimani, aende kumtafuta yule aliyepotea? Naye akipata kumwona, kweli nawaambiani: Atamfurahia kuliko wale tisini na tisa wasiopotea. Vivyo hivyo Baba yenu alioko mbinguni hataki, hawa walio wadogo hata mmoja wao apotee. Ndugu yako akikukosea, nenda kamwonye, wewe na yeye mko peke yenu! Akikusikia, umempata tena ndugu yako. Lakini asipokusikia, chukua pamoja na wewe tena mmoja au wawili! Maana kila shauri limalizike kwa kusemewa na mashahidi wawili au watatu. Naye akikataa kuwasikia hao, waambie wateule wenziwe shauri hilo! Lakini atakapokataa kuwasikia nao wateule, awe kwako kama mtu wa kimizimu au mtoza kodi! Kweli nawaambiani: Lo lote, mtakalolifunga nchini, litakuwa limefungwa hata mbinguni; nalo lo lote, mtakalolifungua nchini, litakuwa limefungwa hata mbinguni; nalo lo lote, mtakalolifungua nchini, litakuwa limefunguliwa hata mbinguni. Tena nawaambiani: Kila jambo, wenzenu wawili nchini watakalopatana kuliomba, watapewa na Baba yangu alioko mbinguni. Kwani watu wawili au watatu wanapolikusanyikia Jina langu, nami nipo hapo katikati yao. *Ndipo, Petero alipomjia, akamwambia: Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi, nikimwondolea? Yatosha mara saba? Yesu akamwambia: Sikuambii: Mwondolee mara saba, ila mwondolee mara sabini mara saba! Kwa sababu hiyo ufalme wa mbingu umefanana na mfalme aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuhesabu akaletewa mmoja mwenye madeni ya mizigo 10000 ya fedha. Naye alipokosa vya kumlipa, bwana akaagiza, wauzwe yeye na mkewe na watoto wake navyo vyote, alivyokuwa navyo, deni lipate kulipika. Mtumwa akamwangukia, akamlalamikia akisema: Nivumilie, nitakulipa yote! Bwana akamwonea uchungu yule mtumwa, akamfungua, akamwachilia hata deni lake. Lakini yule mtumwa alipotoka akamwona mtumwa mwenziwe mmoja aliyekuwa mdeni wake wa shilingi 100. Akamkamata, akamshika koo, akasema: Lipa deni lako! Mtumwa mwenziwe akaanguka miguuni pake, akambembeleza akisema: Nivumilie, nitakulipa! Lakini yule hakutaka, akaenda, akamtia kifungoni, mpaka atakapolilipa lile deni. Basi, watumwa wenziwe walipoyaona yaliyokuwa wakasikitika sana. Wakaja, wakamweleza bwana wao hayo yote yaliyokuwa. Ndipo, bwana wake alipomwita, akamwambia: Wee mtumwa mbaya, lile deni lote nalikuachilia, uliponibembeleza. Wewe nawe haikukupasa kumhurumia mtumwa mwenzio, kama nilivyokuhurumia mimi? Bwana wake akakasirika, akamtoa, afungwe, mpaka atakapolilipa deni lake lote. Ndivyo, naye Baba yangu wa mbinguni atakavyowatendea ninyi, msipoondoleana mioyoni mwenu kila mtu na ndugu yake.* Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo, akaondoka Galilea, akaja mipakani kwa Yudea ng'ambo ya Yordani. Wakamfuata makundi mengi ya watu akawaponya huko. Nao Mafariseo wakamjia, wakamjaribu wakimwuliza: Iko ruhusa, mtu amwache mkewe kwa sababu yo yote? Naye akajibu akisema: Hamkusoma, ya kuwa Muumbaji hapo mwanzo aliwaumba mume na mke, akasema: Kwa sababu hii mtu atamwacha baba yake na mama yake, agandamiane na mkewe, nao hao wawili watakuwa mwili mmoja? Kwa hiyo sio wawili tena, ila wamekuwa mwili mmoja tu. Basi, Mungu alichokiunga, mtu asikiungue! Wakawambia: Mose aliagiziaje tena kuwapa watu cheti cha kuachana, kisha kuwaacha? Akawaambia: kwa ajili ya ugumu wa mioyo yenu Mose aliwapa ruhusa ya kuwaacha wake zenu. Lakini tokea hapo mwanzo havikuwapo hivyo. Nami nawaambiani: Mtu akimwacha mkewe, isipokuwa kwa ajili ya ugoni, akaoa mwingine, anazini; naye anayeoa mke aliyeachwa anazini. Wanafunzi wakamwambia: Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa. Naye akawaambia: Sio wote wanaoweza kuitambua maana yake neno hili, ni wale tu waliofunuliwa. Kwani katika watu wasiozaa, wako waliozaliwa hivyo tangu tumboni mwa mama zao. Tena wako wengine waliokomeshwa na watu, wasizae. Tena wako wengine waliojikomesha wenyewe, wasizae kwa ajili ya ufalme wa mbingu. Anayeweza kuitambua maana na aitambue! Hapo ndipo, alipoletewa vitoto, awabandikie mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi waliwatisha. Ndipo, Yesu aliposema: Waacheni vitoto, msiwazuie kuja kwangu! Kwani walio hivyo ufalme wa mbingu ni wao Akawabandikia mikono; kisha akaondoka pale, akaenda zake. Hapo ndipo mmoja alipomjia na kusema: Mfunzi mwema, nifanye jambo jema gani, niupate uzima wa kale na kale? Naye akamwambia: Unaniulizaje jambo lililo jema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia uzimani yashike maagizo! Alipomwuliza: Yapi? Yesu akasema: Ni haya: Usiue! Usizini! Usiibe! Usisingizie! Mheshimu baba na mama! nalo hilo: Umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwenyewe! Yule kijana akamwambia: Hayo yote nimeyashika; ninalolisaza la kulifanya ni nini tena? Yesu akamwambia: Ukitaka kuyatimiza yote nenda, uviuze, ulivyo navyo, uvigawie maskini! Hivyo utakuwa na kilimbiko mbinguni. Kisha uje, unifuate! Lakini yule kijana alipolisikia neno hili akaenda zake na kusikitika, kwani alikuwa mwenye mali nyingi. Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: Kweli nawaambiani: Ni vigumu, mwenye mali aingie katika ufalme wa mbingu. Tena nawaambiani: Masumbuko ya ngamia ya kupenya tunduni mwa sindano ni madogo kuliko yake mwenye mali ya kuingia ufalme wa Mungu. Wanafunzi walipoyasikia wakastuka sana, wakasema: Ikiwa hivyo, yuko nani awezaye kuokoka? Yesu akawachungua, akawaambia: Kwa watu neno hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana. Hapo Petero akamjibu akimwambia: Tazama, sisi tumeviacha vyote, tukakufuata wewe; basi, tutapata nini? Ndipo, Yesu alipowaambia: Kweli nawaambiani: Siku, ulimwengu utakapopata kuwa mpya, Mwana wa mtu atakapokaa katika kiti cha utukufu wake, hapo ndipo nanyi mlionifuata mimi mtakapokaa katika viti vya kifalme kumi na viwili, myahukumu hayo mashina kumi na mawili ya Isiraeli. Ndipo, kila mtu aliyeacha nyumba au kaka au dada au baba au mama au wana au mashamba kwa ajili ya Jina langu atakapoyapata tena na kuongezwa mara nyingi, kisha ataurithi nao uzima wa kale na kale. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, nao walio wa mwisho watakuwa wa kwanza. *Ufalme wa mbingu umefanana na mtu mwenye numba aliyetoka mapema kutafuta wakulima, wamlimie mizabibu yake. Alipokwisha patana na wakulima mchana kutwa kwa shilingi akawatuma katika mizabibu yake. Ilipopata saa tatu, akatoka, akaona wengine waliosimama sokoni pasipo kazi. Nao akawaambia: Nendeni nanyi katika mizabibu! Nami kinachowapasa nitawapani. Basi, wakaenda. Ilipopata saa sita na saa kenda, akatoka tena, akafanya vilevile. Hata ilipopata saa kumi na moja, akatoka, akaona wengine waliosimama, akawaambia: Mnasimamaje hapa mchana kutwa pasipo kazi? Wakamwambia: Kwa sababu hakuna mtu aliyetuita kazini. Akawaambia: Nendeni nanyi katika mizabibu! Basi ilipokuwa jioni, mwenye mizabibu akamwambia msimamizi wake: Waite wakulima, uwape mshahara wao, uanzie wa mwisho, uishilizie wa kwanza! Wakaja wa saa kumi na moja, wakapokea kila mtu shilingi. Walipokuja wa kwanza wakadhani, ya kuwa watapokea zaidi. Lakini nao wakapokea kila mtu shilingi. Walipoipokea wakamnung'unikia mwenye nyumba wakisema: Hawa wa mwisho wamefanya kazi saa moja tu, nawe umewalinganisha na sisi tuliosumbuka kwa kazi na kwa jua kali mchana kutwa. Naye akamjibu mmoja wao akisema: Mwenzangu, sikukupunja, hukupatana nami kwa shilingi? Chukua iliyo yako, ujiendee! Huyu wa mwisho nataka kumpa kama wewe. Kumbe sina ruhusa ya kufanya na mali yangu mwenyewe, kama nitakavyo? Au jicho lako linakuwa baya, kwa sababu mimi ni mwema? Hivyo ndivyo, walio wa mwisho watakavyokuwa wa kwanza, nao walio wa kwanza watakuwa wa mwisho. Kwani waalikwao ni wengi, lakini wachaguliwao ni wachache tu.* Yesu alipotaka kupanda kwenda Yerusalemu akawachukua wale kumi na wawili, wawe peke yao. Akawaambia njiani: Tazameni tunapanda kwenda Yerusalemu. Huko Mwana wa mtu atatiwa mikononi mwao watambikaji wakuu na waandishi, nao watamhukumu, auawe; kwa hiyo watamtia mikononi mwa wamizimu, wapate kumfyoza na kumpiga viboko na kumwamba msalabani. Naye siku ya tatu atafufuliwa. Ndipo, alipomjia mama yao wana wa Zebedeo pamoja na wanawe, akamwangukia na kumwomba kitu. Alipomwuliza: Wataka nini? akamwambia: Sema, hawa wanangu wawili wakae katika ufalme wako mmoja kuumeni, mmoja kushotoni kwako! Yesu akajibu akisema: Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kukinywa kinyweo, nitakachokinywa mimi? Walipomwambia: Twaweza, akawaambia: Kinyweo changu mtakinywa, lakini kumketisha mtu kuumeni na kushotoni kwangu hii si kazi yangu, ila hupewa walioandaliwa na Baba yangu. Wenzao kumi walipoyasikia wakawakasirikia hao ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, wamjongelee, akasema: Mnajua: wafalme wa mataifa huwatawala, nao wakubwa huwatumikisha kwa nguvu. Kwenu ninyi visiwe hivyo ila mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu sharti awe mtumishi wenu! Naye anayetaka kuwa wa kwanza kwenu sharti awe mtumwa wenu! Kama Mwana wa mtu asivyokuja, atumikiwe, ila amekuja kutumika na kuitoa roho yake kuwa makombozi ya watu wengi. Walipokuwa wakotoka Yeriko, likamfuata kundi la watu wengi. Ndipo, vipofu wawili waliokaa njani kando waliposikia, ya kuwa ni Yesu anayepita, wakapaza sauti wakisema: Bwana, mwana wa Dawidi, tuhurumie! Lakini watu wakawakaripia, wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti wakisema: Bwana, mwana wa Dawidi, tuhurumie! Ndipo, Yesu aliposimama, akawaita, akasema: Mwataka, niwafanyie nini? Wakamwambia: Bwana, twataka, macho yetu yafumbuke! Yesu akawaonea uchungu, akawagusa macho yao. Mara wakapata kuona, wakamfuata. Hapo, walipoukaribia Yerusalemu na kufika Beti-Fage mlimani pa michekele, ndipo, Yesu alipotuma wanafunzi wawili, akawaambia: Nendeni katika kijiji kinachowaelekea! Mara mtaona punda, amefungwa, hata mtoto wake yuko pamoja naye; mfungueni, mniletee! Kama mtu atawaambia neno, mwambieni: Bwana wetu anamtakia kazi! mara atawapani. Haya yote yamekuwapo, lipate kutimizwa neno la mfumbuaji la kwamba: Mwambieni binti Sioni: Tazama, mfalme wako anakujia, ni mpoke, amepanda mwana punda aliye na mama yake, mwenye kuchukua mizigo. Wanafunzi wakaenda, wakafanya, kama Yesu alivyowaagiza. Wakamleta punda na mwanawe, wakatandika nguo juu yao, kisha wakampandisha. Nayo makundi ya watu wengi sana wakatandika nguo zao njiani, wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandika njiani, nao wale watu wengi waliomtangulia, nao waliomfuata wakapaza sauti wakisema: Hosiana, mwana wa Dawidi! Na atukuzwe ajaye kwa Jina la Bwana! Hosiana juu mbinguni!* Alipoingia Yerusalemu, mji wote ukatukutika, wakisema: Nani huyu? Makundi ya watu wakasema: Huyu ndiye mfumbuaji Yesu wa Nasareti wa Galilea. Yesu akapaingia Patakatifu, akawafukuza wote wenye kuuzia na kununulia hapo Patakatifu, akaziangusha meza za wavunja fedha na viti vya wachuuzi wa njiwa, akawaambia: Imeandikwa: Nyumba yangu itaitwa nyumba ya kuombea, lakini ninyi mnaigeuza kuwa pango la wanyang'anyi. Kisha wakamwendea hapo Patakatifu vipofu na viwete, naye akawaponya. Lakini watambikaji wakuu na waandishi walipoyaona mataajabu, aliyoyafanya, tena waliposikia, watoto wakipaza sauti hapo Patakatifu na kusema: Hosiana, mwana wa Dawidi! ndipo, walipokasirika, wakamwambia: Unasikia, hawa wanavyosema? Yesu akawaambia: Ndio. Hamjalisoma bado neno lile la kwamba: Vinywani mwao watoto wachanga namo mwao wanyonyao ulitengeneza tukuzo? Kisha akawaacha, akatoka mjini, akaenda Betania, akalala huko. Asubuhi alipokuwa akirudi mjini akaona njaa. Alipoona mkuyu kando ya njia akauendea, asione kitu kwake, ila majani matupu, akauambia: Kale na kale lisipatikane tena tunda kwako! Mara mkuyu ukawa umenyauka. Wanafunzi walipoviona wakastaajabu, wakasema: Mkuyu huu umenyaukaje mara? Yesu akajibu akiwaambia: Kweli nawaambiani: Mkimtegemea Mungu pasipo mashaka hamtafanya kama hili tu la huu mkuyu, ila hata mkiuambia mlima huu: Ondoka hapa, ulipo, ujitupe baharini! basi itatendeka. Nayo yo yote, mtakayoyaomba katika maombo, mtayapata mkiwa mnamtegemea Mungu. Alipokwisha ingia Patakatifu, akiwa akifundisha, wakamjia watambikaji wakuu na wazee wa huku kwao, wakamwuliza: Hayo unayafanya kwa nguvu gani? Tena ni nani aliyekupa nguvu hii? Yesu akajibu akiwaambia: Hata mimi nitawauliza neno moja; mtakaponijibu neno hilo, basi, hata mimi nitawaelezea nguvu yangu ya kuyafanya hayo. Ubatizo wake Yohana ulikuwa umetoka wapi? Mbinguni au kwa watu? Nao wakafikiri mioyoni mwao kwamba: Tukisema: Ulitoka mbinguni, atatuuliza: Mbona hamkumtegemea? Lakini tukisema: Ulitoka kwa watu, tunawaogopa watu; kwani wote wanamshika Yohana kuwa mfumbuaji. Kwa hiyo wakamjibu Yesu wakisema: Hatujui. Ndipo, alipowaambia: Basi, hata mimi siwaambii nguvu inayonifanyisha hayo. *Lakini mwaonaje? Kulikuwa na mtu mwenye wana wawili. Akamwendea mkubwa, akasema: Mwanangu, nenda leo kufanya kazi mizabibuni! Akamjibu, akasema: Sitaki; lakini halafu alijuta akaenda. Alipomwendea wa pili na kumwambia yaleyale, yeye akajibu akisema: Ndio, bwana; lakini hakuenda. Katika hao wawili aliyeyafanya, baba aliyoyataka, ni yupi? Wakasema: Ni wa kwanza. Yesu akawaambia: Kweli nawaambiani: Watoza kodi na wenye ugoni watawatangulia ninyi kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwani Yohana alikuja kwenu, akafuata njia yenye wongofu, nanyi hamkumtegemea, lakini watoza kodi na wenye ugoni walimtegemea. Lakini ninyi mlipoviona, hata hapo hamkujuta na kumtegemea.* Sikilizeni mfano mwingine! Kulikuwa na mtu mwenye nyumba aliyepanda mizabibu, akaizungusha ugo, akachimbua humo kamulio la kuzikamulia zabibu, akajenga dungu, akaipangisha wakulima, kisha akaenda katika nchi nyingine. Siku za kuiva zabibu zilipotimia, akatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapewe zabibu zake. Nao wakulima wakawakamata watumwa wake, mmoja wakampiga, mmoja wakamwua, mmoja wakamtupia mawe. Akatuma tena watumwa wengine walio wengi kuliko wa kwanza. Wakawatendea vilevile. Mwisho akamtuma mwanawe kwao akisema: Watamcha mwanangu. Lakini wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: Huyu ndiye kibwana, njoni, tumwue, tuupate urithi wake! Kwa kiyo wakamkamata, wakamsukuma sukuma mpaka nje ya mizabibu, wakamwua. Basi, mwenye mizabibu atakapokuja wakulima wale atawafanyia nini? Wakamwambia: Hao wabaya atawaangamiza vibaya, nayo mizabibu atawapangisha wakulima wengine watakaompa zabibu zake, zitakapoiva. *Yesu akawaambia: Hamjasoma katika Maandiko ya kuwa: Jiwe, walilolikataa waashi, hilihili limekuwa la pembeni? Hivyo vimefanywa na Bwana; nasi tukivitazama, ni vya kustaajabu. Kwa sababu hiyo nawaambiani: Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu taifa jingine litakalozaa matunda yake liupate. Naye atakayeanguka juu ya jiwe hilo atapondeka, naye litakayemwangukia, litambana tikitiki*. Watambiakaji wakuu na Mafariseo walipoisikia mifano yake wakatambua, ya kuwa anawasema wao. Kwa hiyo wakatafuta kumkamata, lakini waliwaogopa makundi ya watu, kwani walimwona kuwa mfumbuaji. Yesu akaendelea kusema tena kwa mifano akiwaambia: Ufalme wa mbingu umefanana na mtu mfalme aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa wake, wawaite walioalikwa arusini; nao hawakutaka kuja. Akatuma watumwa wengine akisema: Waambieni walioalikwa: Tazameni, nimekwisha kuiandaa karamu yangu, ng'ombe na vinono vimechinjwa, vyote viko tayari, njoni arusini! Lakini wale wakavibeza, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwa uchuuzi wake. Nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawapiga, wakawaua. Lakini mfalme akachafuka, akawatuma askari wake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Hapo akawaambia watumwa wake: Arusi iko tayari, lakini walioalikwa hawakufaa. Basi, nendeni, mfike kwenye njia panda mwalikie arusini wo wote, mtakaowaona! Wale watumwa wakatoka, wakaenda njiani, wakawakusanya wote, waliowaona, wabaya na wema; arusi ikajaa wageni. Lakini mfalme alipoingia kuwatazama wageni akaona mle mtu asiyevaa nguo inayopasa arusini. Akamwambia: Mwenzangu, uliingiaje humo, nawe hukuvaa nguo inayopasa arusini? Yule akanyamaza kimya. Ndipo, mfalme alipowaambia watumishi: Mfungeni miguu na mikono, mmtupe penye giza lililoko nje! ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno. Kwani waalikwao ni wengi, lakini wachaguliwao ni wachache tu!* Mafariseo wakaenda zao, wakala njama ya kumtega kwa maneno yake. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na watu wa Herode, wakasema: Mfunzi, tumekujua, ya kuwa wewe ni mtu wa kweli, nayo njia ya Mungu unaifundisha, ilivyo kweli, tena humwuliziulizi mtu ye yote, kwani hutazami nyuso za watu. Tuambie, unaonaje wewe? Iko ruhusa ya kumtolea Kaisari kodi au haiko? Kwa kuutambua ubaya wao Yesu akasema: Enyi wajanja, mwanijaribiaje? Nionyesheni fedha ya kodi! Walipomletea shilingi, akawauliza: Chapa hiki cha nani? Maandiko nayo ya nani? Wakasema: Ni yake Kaisari. Ndipo, alipowaambia: Basi, yaliyo yake Kaisari mtoleeni Kaisari, naye Mungu yaliyo yake Mungu! Walipoyasikia wakastaajabu, wakamwacha, wakaenda zao.* Siku ileile wakamjia Masadukeo wanaosema: Hakuna ufufuko, wakamwuliza wakisema: Mfunzi, Mose alisema: Mtu akifa asipokuwa na wana, nduguye amwingilie mkewe, amzalie mkubwa wake mwana! Kwetu kulikuwa na waume saba walio ndugu. Wa kwanza akaoa, akafa; kwa sababu hakuwa na mwana, alimwachia nduguye mkewe. Vilevile na wa pili na wa tatu na wale saba wote. Mwisho wao wote akafa naye mwanamke. Basi, katika ufufuko atakuwa mke wa yupi wa hao saba? Kwani wote waliokuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia: Mwapotelewa, kwani hamyajui Maandiko wala nguvu ya Mungu. Kwani katika ufufuko hawataoa, wala hawataolewa, ila watakuwa, kama malaika walivyo mbinguni. Lakini kwa ajili ya ufufuko wa wafu hamkusoma, mliloambiwa na Mungu aliposema: Mimi ni Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo? Basi, Mungu siye wa wafu, ila wao walio hai. Watu walipoyasikia wakastushwa kwa ufundisho wake. *Mafariseo waliposikia, ya kuwa amewashinda Masafukeo na kuwafumba vinywa, wakakusanyika pamoja. Mmoja wao aliyekuwa mjuzi wa Maonyo yake Mungu akamwuliza kwa kumjaribu akisema: Mfunzi, agizo lililo kubwa katika Maonyo yake Mungu ni lipi? Naye akamwambia: Umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa mawazo yako yote! Hili ndilo agizo lililo kubwa, tena ni la kwanza. Nalo la pili limefanana nalo, ndilo hili: Umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwenyewe! Katika haya maagizo mawili yamo Maonyo yote ya Mungu pamoja na Wafumbuaji. Wao Mafariseo walipokusanyika, Yesu akawauliza akisema: Mwamwonaje Kristo kuwa ni mwana wa nani? Wakamwambia: Wa Dawidi. Akawauliza: Tena Dawidi alimwitaje Bwana kwa nguvu ya Roho aliposema: Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti kuumeni kwangu, mpaka niwaweke adui zako chini miguuni pako? Basi Dawidi akimwita Bwana, anakuwaje mwana wake? Hata mmoja hakuweza kumjibu neno, wala toka siku ile hakuwako mtu aliyejipa moyo wa kumwuliza neno tena.* Kisha Yesu akasema na watu waliokutanika na wanafunzi wake, kwamba: Kitini pa Mose wamekaa waandishi na Mafariseo. Yo yote, watakayowaambia, yafanyeni na kuyashika! Lakini kama wafanyavyo, msiyafuate! Kwani kusema wanasema, lakini hawayafanyi. Huwafungia watu mizigo mizito isiyochukulika wakiwawekea mabegani, lakini wenyewe hawataki kuigusa hata kwa kidole chao kimoja tu. Matendo yao yote huyafanyia kutazamwa na watu. Hukuza makaratasi ya kuombea, huviongeza navyo vishada vya nguo zao, viwe vinene. Wakialikwa chakulani hupenda kukaa penye wakuu, namo nyumbani mwa kuombea hupenda viti vya mbele. Hupenda kuamkiwa na watu sokoni na kuitwa mfunzi mkuu. Lakini ninyi msitake kuitwa mfunzi mkuu! Kwani mfunzi wenu ni mmoja, ndiye Kristo, nanyi nyote ni ndugu. Tena nchini msimwite mtu baba yenu! Kwani baba yenu ni mmoja, ni wa mbinguni. Wala msitake kuitwa kiongozi! Kwani kiongozi wenu ni mmoja, ni Kristo. Lakini kwenu aliye mkubwa na awatumikie ninyi! Kwani atakayejikweza mwenyewe atanyenyekezwa; naye atakayejinyenyekeza mwenyewe atakwezwa. Yatawapata ninyi waandishi na Mafariseo mlio wajanja, kwani mnawafungia watu mlango wa ufalme wa mbingu. Ninyi hamwingii, nao wanaotaka kuingia hamwaachi, waingie. Yatawapata ninyi waandishi na Mafariseo mlio wajanja, kwani mnazila nyumba za wajane mkijitendekeza, kama mnakaza kuwaombea. Kwa hiyo mapatilizo yenu yatakuwa kuliko ya wengine. Yatawapata ninyi waandishi na Mafariseo mlio wajanja, kwani mnazunguka baharini na katika nchi kavu, mpate mfuasi mmoja tu; kisha hapo akipatikana, mnamgeuza kuwa wa kutumbukizwa motoni kuwapita ninyi kabisa. Yatawapata ninyi viongozi vipofu mnaosema: Mtu atakapoapa na kulitaja Jumba la Mungu, si kitu; lakini mtu atakapoapa na kuitaja dhahabu ya Jumba la Mungu amejifunga! Wajinga na vipofu ninyi! Iliyo kubwa ni nini? Dhahabu au Jumba la Mungu linaloitakasa dhahabu? Tena mnasema: Mtu atakapoapa na kuitaja meza ya Bwana, si kitu; lakini atakapoapa na kukitaja kipaji kilichoko juu yake amejifunga! Vipofu ninyi! Iliyo kubwa ni nini? Kipaji au meza ya Bwana inayokitakasa kipaji? Mtu anayeapa na kuitaja meza ya Bwana huapa na kuitaja hiyo meza pamoja navyo vyote vilivyopo pake. Tena mtu anayeapa na kulitaja Jumba la Mungu huapa na kulitaja hilo Jumba pamoja naye yule anayekaa humo. Tena mtu anayeapa na kuitaja mbingu huapa na kukitaja kiti cha kifalme cha Mungu pamoja na yeye anayekikalia. Yatawapata ninyi waandishi na Mafariseo mlio wajanja, kwani fungu la kumi mnalitolea hata mchicha na nyanya na pilipili, lakini yaliyo magumu katika Maonyo mmeyaacha, yale ya hukumu na ya huruma na ya mategemeo. Haya yawapasa kuyashika pasipo kuyaacha yale. Viongozi vipofu ninyi, mbu mnawatema, lakini ngamia mnawameza! Yatawapata ninyi waandishi na Mafariseo mlio wajanja, kwani vinyweo na vyano mnaviosha nje, lakini ndani vimejaa mapokonyo na mapujufu. Fariseo kipofu, kwanza osha ndani yake kinyweo na chano, vipate kuwa safi hata nje! Yatawapata ninyi waandishi na Mafariseo mlio wajanja, kwani mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo huonekana nje kuwa mazuri, lakini ndani hujaa mifupa ya wafu na uchafu wote. Vivyo hivyo nanyi nje mnaonekana kwa watu kuwa waongofu, lakini ndani yenu imejaa ujanja na upotovu. Yatawapata ninyi waandishi na Mafariseo mlio wajanja, kwani mnayajenga makaburi ya wafumbuaji, tena mnayapamba makumbusho ya waongofu na kusema: Sisi kama tungalikuwapo siku za baba zetu, basi, hatungalifanya nao bia ya kuwaua wafumbuaji. Hivyo mnajishuhudia wenyewe, ya kuwa m-wana wao waliowaua wafumbuaji. Nanyi kijazeni kipimo cha baba zenu! M nyoka, m wana wa chatu! Mtaikimbiaje hukumu ya kutumbukizwa shimoni mwa moto? *Kwa sababu hii tazameni, mimi natuma kwenu wafumbuaji na werevu wa kweli na waandishi; wengine wao mtawaua na kuwawamba misalabani, wengine wao mtawapiga katika nyumba zenu za kuombea, kisha mtawafukuza mji kwa mji; hivyo zitawajia damu zote za waongofu zilizomwagwa nchini, kuanzia damu ya Abeli aliyekuwa mwongofu mpaka kuifikia damu ya Zakaria, mwana wa Berekia, mliyemwua katikati ya Jumba la Mungu na meza ya Bwana. Kweli nawaambiani: hayo yote yatawajia wao wa kizazi hiki. Yerusalemu, Yerusalemu, unawaua wafumbuaji, ukawapiga mawe walitumwa kwako! Mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako, kama kuku anavyovikusanya vifaranga vyake mabawani! Lakini hamkutaka! Mtaona, Nyumba yenu ikiachwa, iwe peke yake! Kwani nawaambiani: Tangu sasa hamtaniona tena, mpaka mtakaposema: Na atukuzwe ajaye kwa Jina la Bwana!* Yesu alipotika Patakatifu akaenda zake. Wakamjia wanafunzi wake, wakamwonyesha majengo ya hapo Patakatifu; ndipo, alipojibu akiwaambia: Je? Mwayatazama haya yote? Kweli nawaambiani: Hapa halitaachwa hata jiwe moja juu ya jiwe lenziwe lisiloporomoshwa chini. Kisha alipokaa mlimani pa michekele, wanafunzi wakamjia; walipokuwa peke yao wakasema: Tuambie, hayo yatakuwapo lini? Tena kielekezo cha kurudi kwako na cha mwisho wa dunia ni nini? Yesu akajibu akiwaambia: Angalieni, mtu asiwapoteze! Kwani wengi watakuja kwa jina langu na kusema: Mimi ni Kristo; nao watapoteza wengi. Tena mtasikia vita na mavumi ya vita; vitazameni tu, msivihangaikie! Kwani hivyo sharti viwepo, lakini huo sio mwisho. Kwani watainukiana taifa na taifa, tena wafalme na wenzao wafalme; mahali penginepengine patakuwa na kipundupindu, pengine na njaa, pengine na matetemeko. Lakini hayo yote ni mwanzo tu wa uchungu. Hapo watatoa ninyi, mpate kuumizwa, hata kuuawa, tena mtachukiwa na makabila yote kwa ajili ya Jina langu. Hapo ndipo, wengi watakapokwazwa, watoane wenyewe kila mtu na mwenziwe kwa kuchukiana wao kwa wao. Hata wafumbuaji wa uwongo wengi watainuka na kupoteza wengi. kwa sababu upotovu utazidi kuwa mwingi, upendo wa wengi utapoa. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka. Nao huu utume mwema wa ufalme wa Mungu utatangawa ulimwenguni mote, uje, unishuhudie kwa wamizimu wote. Kisha ndipo, mwisho utakapokuja. *Hapo ndipo, mtakapochafukwa mioyo mkiona, mwangamizaji atapishaye akisimama mahali Patakatifu, kama mfumbuaji Danieli alivyosema; mwenye kupasoma hapa sharti aangalie, ajue maana! Siku zile watakaokuwako Yudea na wakimbilie milimani! Mtu atakayekuwapo nyumbani juu asishuke kuvichukua vilivyomo nyumbani mwake! Naye atakayekuwako shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake! Lakini watakaoona vibaya zaidi ndio wenye mimba na wenye kunyonyesha siku zile. Lakini ombeni, kukimbia kwenu kusitimie siku za kipupwe wala siku ya mapumziko! Kwani hapo patakuwa na maumivu makuu kuyapita yote yaliyopatikana tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka sasa, hata halafu hayatapatikana tena kama hayo. Nazo siku zile kama hazingalipuinguzwa, hangaliokoka mtu hata mmoja. Lakini kwa ajili ya wale waliochaguliwa siku zile zitapunguzwa. Hapo mtu akiwaambia: Tazama, huyu hapa ni Kristo! au akisema: Yule kule! msiitikie! Kwani watainuka makristo wa uwongo na wafumbuaji wa uwongo; nao watatoa vielekezo vikubwa na vioja, wawapoteza hata waliochaguliwa, kama inawezekana. Tazameni, nimetangua kuwaambia ninyi. Basi, watakapowaambia ninyi: Tazameni, yuko jangwani! msitoke kwenda kule! Au: Yule! Yumo nyumbani! msiitikie! Kwani kama umeme unavyotoka maawioni, ukamulika mpaka machweoni, ndivyo, kutakavyokuwa kurudi kwake Mwana wa mtu. Penye nyamafu ndipo, tai watakapokusanyikia.* Maumivu ya siku zile yatakapopita, papo hapo jua litakuwa jeusi lenye giza, nao mwezi hautaumulikisha mwanga wake, nazo nyota zitaanguka toka mbinguni, nazo nguvu za mbingu zitatukutishwa. Hapo ndipo, patakapoonekana mbinguni kielekezo cha Mwana wa mtu. Ndipo, watakapoomboleza wao wa makabila yote ya nchi, watakapomwona Mwana wa mtu, anavyokuja juu ya mawingu toka mbinguni mwenye nguvu na utukufu mwingi. Naye atawatuma malaika zake wenye mabaragumu yanayolia sana, wawakusanye waliochaguliwa naye toka pande zote nne, upepo unapotokea, waanzie mwanzoni kwa mbingu, waufikishe mwisho wake. Jifundisheni mfano kwa mkuyu: matawi yake yanapochipua na kuchanua majani, mnatambua, ya kuwa siku za vuli ziko karibu. Vivyo hivyo nanyi mtakapoyaona hayo yote tambueni, ya kuwa mwisho umewafikia milangoni! Kweli nawaambiani: Kizazi hiki hakitakoma, mpaka yatakapokuwapo hayo yote. Mbingu na nchi zitakoma, lakini maneno yangu hayatakoma. Lakini ile siku na saa yake itakapofikia, mtu hapajui, wala malaika wa mbingu, wala Mwana, ila Baba peke yake tu. Kama vilivyokuwa siku za Noa, ndivyo kutakavyokuwa kurudi kwake Mwana wa mtu. Kwani siku zile zilizoyatangulia yale mafuriko makubwa ya maji walikuwa wakila, hata wakinywa, wakioa, hata wakiozwa mpaka siku, Nao alipoingia katika chombo kikubwa. Hawakuyatambua, mpaka mafuriko makubwa ya maji yakaja, yakawachukua wote pia. Ndivyo, kutakavyokuwa hata kurudi kwake mwana wa mtu. Hapo wawili watakuwa shambani, mmoja atapokewa, mmoja ataachwa. Hapo wawili watakuwa shambani, mmoja atapokewa, mmoja ataachwa. Kwa hiyo kesheni! Kwani hamwijui siku, atakapojia Bwana wenu. Lakini litambueni neno hili: Kama mwenye nyumba angaliijua zamu, mwizi atakayojia, angalikesha, asiache, nyumba yake ibomolewe. Kwa sababu hiyo nanyi mwe tayari! Kwani Mwana wa mtu atajia saa, msiyomwazia. Basi, yuko nani aliye mtumwa mwelekevu na mwerevu, bwana wake akimpa kuwatunza wa nyumbani mwake, awape vyakula, saa yao itakapofika? Mwenye shangwe ni mtumwa yule, bwana wake atakayemkuta, akifanya hivyo, atakapokuja. Kweli nawaambiani: Atampa kuzitunza mali zake zote. Lakini mtumwa aliye mwovu atasema moyoni mwake: Bwana wangu anakawia, akaanza kuwapiga watumwa wenziwe na kula na kunywa pamoja na walevi. Basi, bwana wake mtumwa yule atamjia siku, asiyomngojea, na saa, asiyoitambua, kisha atamchangua kuwa vipande viwili, nalo fungu lake atampa pamoja na wajanja. Ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno. *Hapo ufalme wa mbingu utafanana na wanawali kumi walioshika taa zao, wakatoka kwenda kumpokea bwana arusi. Watano wao walikuwa wajinga, wenzao watano walikuwa werevu. Kwani wale wajinga walizishika taa zao tu, wasichukue na mafuta. Lakini wale werevu walichukua mafuta katika vichupa pamoja na taa zao. Bwana arusi alipokawia, wakasinzia wote, wakalala usingizi. Kati ya usiku pakawa na kelele: Tazameni, bwana arusi huyo! Tokeni, mmpokee! Ndipo, wanawali wale wote walipoinuka, wakazitengeneza taa zao. Lakini wajinga wakawaambia wenzao werevu: Tugawieni mafuta yenu! kwani taa zetu zinazimika. Lakini wale werevcu wakajibu wakisema: Sivyo, hayatatutosha sisi na ninyi; sharti mwende kwa wachuuzi, mjinunulie wenyewe! Walipokwenda kununua, bwana arusi akafika, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini, kisha mlango ukafungwa. Halafu wakaja nao wanawali wale wengine wakasema: Bwana, Bwana, tufungulie! Lakini akajibu akisema: Kweli nawaambiani: Siwajui ninyi. Kwa hiyo kesheni! Kwani hamwijui siku wala saa, Mwana wa mtu atakapojia.* Kwani vinafanana na mtu aliyefunga safari, akawaita watumwa wake mwenyewe, akawapa mali zake kuzitunza. Akampa kila mtu fungu, aliwezalo mwenyewe kulitunza, mmoja fedha elfu tano, mmoja elfu mbili, mmoja elfu moja, kisha akaenda zake. Yule aliyepokea elfu tano akaenda, akazichuuzia, akachuma nazo nyingine elfu tano. Vile vile na yule aliyepokea elfu mbili, naye akachuma nazo nyingine elfu mbili. Lakini yule aliyepokea elfu moja akaenda, akachimba shimo, akazifukia mle fedha za bwana wake. Siku zilipopita nyingi, akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. Akaja yule aliyepokea elfu tano, akaleta elfu tano nyingine akasema: Bwana, umenipa elfu tano; tazama, nimechuma elfu tano nyingine. Bwana wake akamwambia: Vema, wewe mtumwa mwema na mwelekevu, ulikuwa mwelekevu wa machache, nitakupa kutunza mengi. Ingia penye furaha ya bwana wako! Akaja na yule aliyepokea elfu mbili, akasema: Bwana, umenipa elfu mbili. Tazama, nimechuma elfu mbili nyingine. Bwana wake akamwambia: Vema, wewe mtumwa mwema na mwelekevu, ulikuwa mwelekevu wa machache, nitakupa kutunza mengi. Ingia penye furaha ya bwana wako! Akaja na yule aliyekuwa amepokea elfu moja, akasema: Bwana, nalitambua, ya kuwa wewe u mkorofi; huvuna, usipopanda, hukusanya, usipotandaza. Nikaogopa, nikaenda, nikazifukia fedha zako shimoni. Tazama, hizi mali zako, uzichukue! Lakini bwana wake akajibu akimwambia: Mtumwa mbaya wewe! U mvivu! Ulinijua, ya kuwa navuna, nisipopanda, nakusanya nisipotandaza? Basi, ilikupasa kuziweka fedha zangu kwao wenye maduka, nami nilipokuja ningalizichukua zilizo zangu pamoja na faida. Kwa hiyo ichukueni elfu yake ya fedha, mmpe mwenye elfu kumi! Kwani kila mwenye mali atapewa, ziwe nyingi zaidi; lakini asiye na kitu atachukuliwa hata kile, alicho nacho. Lakini huyu mtumwa asiyefaa mtupeni penye giza lililoko nje! Ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno. *Hapo, atakapokuja Mwana wa mtu mwenye utukufu wake na malaika wote pamoja naye, ndipo, atakapokalia kiti cha utukufu wake, nayo mataifa yote yatakusanywa mbele yake; naye atawabagua, kama mchungaji anavyowabagua kondoo na mbuzi. Atawaweka kondoo kuumeni kwake, nao mbuzi kushotoni. Hapo mfalme atawaambia walioko kuumeni kwake: Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme, mliotengenezewa tangu hapo, ulimwengu ulipoumbwa! Kwani nilipokuwa na njaa, mlinipa chakula; nilipokuwana kiu, mlininywesha; nilipokuwa mgeni, mlinipokea; nilipokuwa uchi, mlinivika; nilipokuwa mgonjwa, mlinikagua; nilipokuwa kifungoni mlinijia. Ndipo wale waongofu watakapomjibu: Bwana, ni lini, tulipokuona na njaa, tukakulisha? Au tulipokuona na kiu, tukakunywesha? Tena ni lini, tulipokuona mgeni, tukakupokea? Au tulipokuona uchi, tukakuvika? Ni lini tena, tulipokuona mgonjwa au kifungoni, tukakujia? Naye mfalme atawajibu akisema: Kweli nawaambiani: Yote, mliyomtendea mwenzao mmoja wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi. Kisha atawaambia walioko kushotoni: Ondokeni kwangu, mlioapizwa, mwingie kwenye moto usiozimika, uliowashiwa Satani na malaika zake! Kwani nilipokuwa na njaa, hamkunipa chakula; nilipokuwa na kiu, hamkuninywesha; nilipokuwa mgeni, hamkunipokea; nilipokuwa uchi, hamkunivika; nilipokuwa mgonjwa na kifungoni, hamkuja kunikagua. Ndipo, nao wale watakapojibu wakisema: Bwana, ni lini, tulipokuona na njaa au na kiu au mgeni au mwenye uchi au mgonjwa au kifungoni, tusikutumikie? Hapo atawajibu akisema: Kweli nawaambiani: Yote, msiyomtendea mwenzao mmoja tu wa hawa ndugu zangu wadogo, basi hamkunitendea hata mimi. Kisha hawa watakwenda kuingia penye maumivu ya kale na kale. Lakini wale waongofu watakwenda kuingia penye uzima wa kale na kale.* Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo yote, akawaambia wanafunzi wake: Mmejua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka; naye Mwana wa mtu atatolewa, awambwe msalabani. Hapo watambikaji wakuu na wazee wa huko kwao wakakusanyika nyumbani mwa mtambikaji mkuu, jina lake Kayafa, wakala njama ya kumkamata Yesu kwa werevu wapate kumwua. Lakini walisema: Kwanza sikukuu ipite, watu wasije, wakafanya fujo! Yesu alipokuwa Betania nyumbani mwa Simoni Mkoma, akamjia mwanamke mwenye kichupa cheupe cha jiwe kilichojaa mafuta ya maua yaliyo yenye bei kubwa. Akammiminia kichwani pake, alipokaa akila. Lakini wanafunzi walipoviona wakachukiwa, wakasema: Upotevu huu ni wa nini? Kwani mafuta haya yangaliwezekana kuuzwa kwa fedha nyingi, wakapewa maskini. Lakini Yesu alipovitambua, akawaambia: Mbona mnamsikitisha mwanamke huyu? Maana amenitendea tendo zuri. Kwani maskini mnao kwenu siku zote, lakini mimi hamwi nami siku zote. Kwani alipoyamimina mafuta haya, aupake mwili wangu, ameutengenezea kuzikwa. Kweli nawaambiani: Po pote katika ulimwengu wote, patakapotangazwa Utume huu mwema, patasemwa nacho hiki, alichokitenda yeye, naye akumbukwe. Hapo wale kumi na wawili mwenzao mmoja aliyeitwa Yuda Iskariota akaenda kwa watambikaji wakuu, akasema: Mwataka kunipa nini, nitakapomtia mikononi mwenu? Wakaagana kumpa fedha 30. Toka hapohapo alitafuta njia iliyofaa amtoe. Siku ya kwanza ya kula mikate isiyotiwa chachu wanafunzi wakamjia Yesu wakisema: Unataka, tukuandalie wapi, uile kondoo ya Pasaka? Naye akasema: Nendeni mjini kwa fulani, mmwambie: Mfunzi anasema: Siku zangu zinatimia! Kwako nitaila kondoo ya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya, kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa kondoo ya Pasaka. Ilipokuwa jioni, akakaa chakulani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakila, akasema: Kweli nawaambiani: Mwenzenu mmoja atanichongea. Wakasikitika sana, wakaanza kumwuliza kila mmoja: Bwana, ni mimi? Naye akajibu akisema: Aliyetowelea pamoja nami bakulini ndiye atakayenichongea. Mwana wa mtu anakwenda njia yake, kama alivyoandikiwa; lakini yule mtu, ambaye Mwana wa mtu atachongewa naye, atapatwa na mambo. Ingalimfalia yule mtu, kama asingalizaliwa. Ndipo, Yuda aliyemchongea alipomwuliza akisema: Mfunzi mkuu, ni mimi? Akamjibu: Ndio umesema. Walipokuwa wakila, Yesu akatwaa mkate, akauombea, akaumega, akawapa wanafunzi akisema: Twaeni, mle! Huu ndio mwili wangu. Kisha akatwaa kinyweo, akashukuru, akawapa akisema: Nyweni nyote humu! Maana hii ndiyo damu yangu ya Agano Jipya inayomwagwa kwa ajili ya wengi, wapate kuondolewa makosa. Lakini nawaambiani: Tangu sasa sitayanywa tena mazao ya mizabibu mpaka siku ile, nitakapoyanywa mapya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu. Walipokwisha kuimba wakatoka kwenda mlimani pa michekele. Hapo Yesu akawaambia: Usiku huu wa leo ninyi nyote mtajikwaa kwangu kwani imeandikwa: Nitampiga mchungaji, kondoo wa kundi lake watawanyike; lakini nitakapokwisha kufufuliwa nitawatangulia kwenda Galilea. Ndipo, Petero alipojibu akimwambia: Ijapo wote wajikwae kwako, lakini mimi sitajikwaa kamwe. Yesu akamwambia: Kweli nakuambia: Usiku huu wa leo jogoo atakapokuwa hajawika, utakuwa umenikana mara tatu. Petero akamwambia: Hata ijaponipasa kufa pamoja nawe, sitakukana kabisa. Nao wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo. Kisha Yesu akaenda pamoja nao mahali panapoitwa Getisemane. Akawaambia wanafunzi: Kaeni hapa, niende kule, niombe! Akamchukua Petero na wale wana wawili na Zebedeo, akaanza kusikitika na kuhangaika, akawaambia: Roho yangu inaumizwa sana na masikitiko, imesalia kufa tu. Kaeni papa hapa, mkeshe pamoja nami! Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema: Baba, ikiwezekana kinyweo hiki kinipite, nisikinyuwe! Lakini yasifanyike, kama nitakavyo mimi, ila yafanyike kama utakavyo wewe! Alipowajia wanafunzi, akawakuta, wamelala usingizi, akamwambia Petero: Hamkuweza kukesha pamoja nami saa moja tu? Kesheni na kuomba, msije kuingia majaribuni! Roho inataka kuitikia, lakini mwili ni mnyonge. Akaenda tena mara ya pili, akaomba akisema: Baba, isipowezekana, hiki kinipite, nisikinywe, basi, uyatakayo wewe na yafanyike! Alipokuja tena, akawakuta, wamelala usingizi, kwani macho yao yalikuwa mazito. Akawaacha, akaenda tena, akaomba mara ya tatu akisema tena maneno yale yale. Kisha akawajia wanafunzi, akawaambia: Mwafuliza kulala usingizi, uchovu uwatoke? Tazameni, saa iko karibu, Mwana wa mtu atiwe mikononi mwa wakosaji! Inukeni, twende! Tazameni, mwenye kunichongea yuko karibu! Angali akisema, mara akaja Yuda, mmoja wao wale kumi na wawili, pamoja na watu wengi sana wenye panga na rungu waliotoka kwa watambikaji wakuu na kwa wazee wa huko kwao. Lakini mwenye kumchongea alikuwa amewapa kielekezo akisema: Nitakayemnonea ndiye, mkamateni! Mara akamjia Yesu, akasema: Salamu, mfunzi mkuu! Akamnonea. Yesu akamwambia: Mwenangu, umejia nini? Ndipo, walipokuja, wakamkamata Yesu kwa mikono yao, wakamfunga. Papo hapo wale waliokuwako pamoja na Yesu mmoja wao akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumwa wa mtambikaji mkuu, akamkata sikio. Ndipo, Yesu alipomwambia: Urudishe upanga wako mahali pake! kwani wote wenye kushika panga wataangamizwa kwa upanga. Au unadhani: Siwezi kumbembeleza Baba yangu, naye akaniletea sasa hivi malaika wengi kupita elfu kumi na mbili? Lakini Maandiko yangetimizwaje yale ya kwamba, sharti yawe vivyo hivyo? Saa ile Yesu akawaambia yale makundi ya watu: Mmetoka wenye panga na rungu, mnikamate mimi, kama watu wanavyomwendea mnyang'anyi. Kila siku nilikaa hapa Patakatifu nikifundisha, lakini hamkunikamata. Lakini haya yote yamekuwapo, Maandiko ya Wafumbuaji yatimizwe. Papo hapo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Lakini wale waliomkamata Yesu wakampeleka kwa mtambikaji mkuu Kayafa; ndiko, walikokusanyika waandishi na wazee. Lakini Petero akamfuata mbalimbali, mpaka akafika uani kwa mtambikaji mkuu, akaingia ndani akakaa pamoja na watumishi, uone mwisho. Lakini watambikaji wakuu na baraza ya wakuu wote wakamtafutia Yesu ushuhuda wa uwongo, wapate kumwua. Lakini hawakuupata, ingawa walikuja mashahidi wa uwongo wengi, lakini hawakumshinda. Halafu wakaja wawili, wakasema: Huyu amesema: Nina nguvu ya kulivunja Jumba la Mungu na kulijenga tena muda wa siku tatu. Ndipo, mtambikaji mkuu alipoinuka, akamwambia: Hujibu neno, hawa wanayokusimangia? Lakini Yesu akanyamaza kinya. Mtambiakaji mkuu akamwambia: Ninakuapisha na kumtaja Mungu Mwenye uzima, utuambie, kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu! Yesu akamwambia: Wewe ulivyosema, ndivyo. Tena nawaambiani: Tangu sasa mtamwona Mwana wa mtu, anavyokaa kuumeni kwa nguvu, tena atakavyokuja juu ya mawingu ya mbinguni. Ndipo, mtambikaji mkuu alipozirarua nguo zake, akasema: Amekwisha kumbeza Mungu. Mashahidi tunawatakia nini tena? Tazameni, sasa hivi mmesikia, anavyombeza Mungu. Mwaonaje? Nao wakajibu, wakasema: Amepaswa na kufa. Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makonde; wengine wakampiga makofi wakisema: Tufumbulie, Kristo: ni nani aliyekupiga? Naye Petero alikuwa nje, amekaa uani. Kijakazi mmoja akamjia, akasema: Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilea. Akakana mbele yao wote akisema: Sijui unayoyasema. Alipotoka uani na kufika mlangoni, mwingine akamwona, akawaambia wale waliokuwako: Huyu alikuwa pamoja na Yesu na Nasareti. Akakana tena na kuapa akisema: Simjui mtu huyo. Punde kidogo wakamjia Petero waliosimama pale, wakamwambia: Kweli, na wewe u mwenzao, kwa maana matamko yako yanakutambulisha. Ndipo, alipoanza kujiapiza na kuapa akisema: Simjui mtu huyo! Mara hiyo jogoo akawika. Hapo Petero akalikumbuka lile neno la Yesu, aliposema: Jogoo atakapokuwa hajawika, utakuwa umenikana mara tatu. Akatoka nje, akalia sana kwa uchungu. Ilipokuwa asubuhi, watambikaji wakuu wote na wazee wa kwao wakamlia Yesu njama, kwamba wamwue. Wakamfunga, wakaenda naye, wakamtia mikononi mwa Pilato aliyekuwa mtawala nchi. Hapo Yuda aliyemchongea akamwona, ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, akajuta, akazirudisha zile fedha 30 kwa watambikaji wakuu na kwa wazee akisema: Nimekosa nilipotoa mtu asiyepaswa na kumwagwa damu yake. Wale wakasema: Jambo hilo hatumo, litazame mwenyewe! Ndipo, alipozitupa zile fedha Jumbani mwa Mungu, akaondoka, akaenda zake, akajinyonga. Kisha watambikaji wakuu wakaziokota zile fedha, wakasema: Ni mwiko kuzitia katiaka sanduku ya vipaji, kwa kuwa ni fedha za damu. Wakazipigia shauri, wakazinunua shamba la mfinyanzi, liwe la kuzikia wageni. Kwa hiyo shamba lile linaitwa hata leo Shamba la Damu. Ndipo, yalipotimia, mfumbuaji Yeremia aliyoyasema: Wamezichukua fedha 30, ni upato wa mtu aliyeuzwa, waliomnunua kwa wana wa Isiraeli; wakazitoa kununua shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniambia. Yesu alipopelekwa mbele ya mtawala nchi, mtawala nchi akamwuliza akisema: Wewe ndiwe mfalme wa Wayuda? Yesu akamwambia: Wewe unavyosema, ndivyo. Tena aliposutwa nao watambikaji wakuu na wazee hakujibu neno. Pilato alipomwambia: Husikii yote, wanayokusimangia? hakumjibu hata neno moja. Ikawa, mtawala nchi akastaajabu sana. *Kwa desturi ya sikukuu mtawala nchi alikuwa amezoea kuwafungulia mfungwa mmoja, watu wengi waliyemtaka. Siku zile palikuwa na mfungwa aliyejulikana kwa ubaya, jina lake Baraba. Walipokusanyika, Pilato akawauliza: Mwamtaka yupi, niwafungulie? Baraba au Yesu anayeitwa Kristo? Kwani aliwajua, ya kuwa wamemtoa kwa wivu. Naye alipoketi katika kiti cha uamuzi, mkewe akatuma kwake kumwambia: Usijitie katika jambo la yule mwongofu! Kwani nimeteseka mengi kwa ajili yake katika ndoto za usiku wa leo. Lakini watambikaji wakuu na wazee wakawashurutisha makundi ya watu, wamtake Baraba, wamwangamize Yesu. Mtawala nchi akajibu akiwaambia: Katika hawawawili mwamtaka yupi, niwafungulie? Wakasema: Baraba! Pilato akamwambia: Basi, Yesu anayeitwa Kristo nimfanyie nini? Wakasema wote: Na awambwe msalabani! Aliposema: Ni kiovu gani, alichokifanya? wakakaza kupiga makelele wakisema: Na awambwe msalabani! Pilato alipoona, ya kama hakuna linalofaa, ila matata yatakuwako mengi, akatwaa maji, akanawa mikono yake machoni pa watu, akasema: Mimi simo katika damu ya mtu huyu mwongofu, tazameni, ni shauri lenu! Ndipo, watu wote walipojibu wakisema: Damu yake itujie sisi na watoto wetu! Kisha akawafungulia Baraba, lakini Yesu akamtoa, apigwe viboko, kisha awambwe msalabani. Ndipo, askari wa mtawala nchi walipompeleka Yesu bomani, wakakita kikosi chote cha askari, waje hapo, alipokuwa. Wakamvua nguo zake, wakamvika kanzu nyekundu ya kifalme. Wakasuka kilemba cha miiba, wakamvika kichwani, wakampa mwanzi mkononi mwake mwa kuume, wakampigia magoti, wakamfyoza na kusema: Pongezi, mfalme wa Wayuda! Kisha wakamtemea mate, wakaushika ule mwanzi, wakampiga kichwani. Walipokwisha kumfyoza wakamvua kanzu ya kifalme, wakamvika tena nguo zake, wakampeleka, wamwambe msalabani.* Walipotoka wakaona mtu wa Kirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha, amchukulie msalaba wake. Walipofika mahali panapoitwa Golgota, maana yake: Fuvu la Kichwa, wakampa mvinyo iliyochanganyika na maji ya nyongo, anywe. Naye alipoyaonja hakutaka kunywa. Walipokwisha kumwamba msalabani wakazigawanya nguo zake na kuzipigia kura, kusudi yatimie yaliyosemwa na mfumbuaji kwamba: Wakajigawanyia nguo zangu, nalo vazi langu wakalipigia kura. Wakakaa wakimlinda palepale. Juu ya kichwa chake wakabandika andiko la mashtaka yake ya kwamba: HUYU NI YESU, MFALME WA WAYUDA. Pamoja naye wakawambwa misalabani wanyang, anyi wawili, mmoja kuumeni, mmoja kushotoni. Waliopita wakamtukana, wakavitingisha vichwa vyao wakisema: Wewe unayelivunja Jumba la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe! Ukiwa Mwana wa Mungu shuka msalabani! Vilevile nao watambikaji wakuu pamoja na waandishi na wazee wakamfyoza wakisema: Wengine aliwaokoa, lakini mwenyewe hawezi kujiokoa. Kama ndiye mfalme wa Waisiraeli, ashuke sasa hivi msalabani! Ndivyo, tutakavyomtegemea nasi. Alimtegemea Mungu, na amwokoe sasa, kama anamtaka! kwani alisema: Mimi ni Mwana wa Mungu. Vivyo hivyo wakamtukana hata wale wanyang'anyi waliowambwa misalabani pamoja naye. Tangu saa sita pakawa na giza katika nchi yote mpaka saa tisa. Ilipokuwa kama saa tisa, Yesu akapaza sauti sana akisema: Eli, Eli, lama sabaktani? Ni kwamba: Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Wengine wao waliosimama hapo walipoyasikia wakasema: Huyu anamwita Elia. Papo hapo mmoja wao akapiga mbio, akachukua mwani, akauchovya sikini na kuutia katika utete, akamnywesha. Wengine wakasema: Acha, tuone, kama Elia anakuja kumwokoa! Kisha Yesu akapaza tena sauti sana, akakata roho. Papo hapo ndipo, pazia la Jumbani mwa Mungu lilipopasuka toka juu mpaka chini, likawa vipande viwili. Nchi ikatetemeka, miamba ikapasuka, makaburi yakafunuka, ikafufuka miili mingi ya watu watakatifu waliolala, wakatoka makaburini mwao, yeye alipokwisha kufufuka, wakauingia mji mtakatifu, wakatokea wengi, wawaone. Lakini bwana askari nao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoliona lile tetemeko na yale mambo yaliyokuwapo, wakaogopa sana, wakasema: Kweli, huyu alikuwa Mwana wa Mungu! Pale palikuwa na wanawake wengi, walisimama mbali wakitazama; ndio waliomfuata Yesu toka Galilea wakimtumikia. Kati yao walikuwapo Maria Magadalene na Maria, mama yao Yakobo na Yosefu, tena mama yao wana wa Zebedeo. Ilipokuwa jioni, akaja mtu mwenye mali nyingi wa Arimatia, jina lake Yosefu; naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu. Huyo akaenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu; ndipo, Pilato alipoagiza, apewe. Yosefu akauchukua ule mwili, akaufunga kwa sanda nyeupe, akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani. Akafingirisha jiwe kubwa mlangoni pa kaburi, akaenda zake. Nao akina Maria Magadalene na Maria yule mwingine, walikuwa wamekaa hapa wakilielekea kaburi. Kulipokucha, ni siku inayofuata maandalio ya kondoo ya Pasaka, watambikaji wakuu na Mafariseo wakamkusanyikia Pilato, wakamwambia: Bwana, tumekumbuka, ya kuwa yule mdanganyifu alisema alipokuwa anaishi bado: Baada ya siku tatu nitafufuka. Kwa hiyo agiza, kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu, wanafunzi wake wasije, wamwibe, wakawaambia watu: Amefufuka katika wafu! madanganyo hayo ya mwisho yakawa mabaya kuliko yale ya kwanza. Pilato akawaambia: Chukueni askari wa kulinda! Nendeni, mkalilinde kaburi, kama mnavyojua! Nao wakaenda, wakaitia muhuri yao juu ya lile jiwe, wakawaweka askari hapo, walilinde kaburi. *Siku ya mapumziko ilipokwisha, siku ya kwanza ya juma kulipokucha, wakaenda Maria Magdalena na yule Maria mwingine kulitazama kaburi. Mara kukawa na tetemeko kubwa la nchi. Kwani malaika wa Bwana alishuka toka mbinguni, akaja akalifingirisha lile jiwe, likatoka mlangoni, akalikalia. Sura yake ilikuwa kama umeme, nguo zake zikang'aa kama chokaa juani. Walinzi wakaingiwa na woga, wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akawaambia wale wanawake akisema: Msiogope! Kwani ninajua, ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyewambwa msalabani. Hayumo humu, kwani amefufuliwa, kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali, Bwana alipokuwa amewekwa! Nanyi nendeni upesi, mwaambie wanafunzi wake kwamba: Amefufuliwa katika wafu! Tazameni, anawatangulia ninyi kwenda Galilea. Huko ndiko, mtakakomwona. Tazameni, nimekwisha kuwaambia. Wakatoka upesi kaburini wakishikwa na woga, tena wakifurahi sana, wakaenda mbio kuwasimulia wanafunzi wake. Mara Yesu akakutana nao, akasema: Salamu kwenu! Nao wakamjia, wakamshika miguu yake, wakamwangukia. Ndipo, Yesu alipowaambia: Msiogope, nendeni, mwasimulie ndugu zangu, waende Galilea! Ndiko, watakakoniona.* Walipokwenda zao, mara nao walinzi wakafika mjini mmoja mmoja, wakasimulia watambikaji wakuu yote yaliyokuwapo. Wakakusanyika pamoja na wazee, wakala njama, wakatoa fedha nyingi za kuwapa wale askari, wakawaambia: Semeni: Wanafunzi wake wamekuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala! Neno hili likijulikana kwa mtawala nchi, sisi tutasema naye kwa werevu, ninyi msipate mahangaiko. Kwa hiyo wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Nalo neno hili linasimuliwa kwa Wayuda mpaka leo. *Wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilea, wakafika mlimani pale, Yesu alipowaagizia. Walipomwona wakamwangukia, lakini wengine waliingiwa na mashaka. Naye Yesu akawajia, akawaambia: Nimepewa nguvu zote mbinguni na nchini. Nendeni, mkawafundishe wao wa mataifa yote, wawe wanafunzi wangu, mkiwabatizia Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu na kuwafundisha, wayashike yote, niliyowaagiza! Tazameni, niko pamoja nanyi siku zote, mpaka dunia itakapokoma.* Utume mwema wa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ulianza, kama ulivyoandikwa na mfumbuaji Yesaya: Utaniona mimi, nikimtuma mjumbe wangu, akutangulie, aitengeneze njia yako. Iko sauti ya mtu apigaye mbiu nyikani: Itengenezeni njia ya Bwana! Yanyosheni mapito yake! Yohana Mbatizaji alikuwa nyikani akibatiza na kutangaza ubatizo wa kujutisha, wapate kuondolewa makosa. Wakamtokea wote wa Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu, wakabatizwa naye katika mto wa Yordani wakiyaungama makosa yao. Naye Yohana alikuwa amevaa nguo ya manyoya ya ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni pake, akala nzige na asali ya mwituni. Akatangaza akisema: Nyuma yangu anakuja aliye na nguvu kunipita mimi, nami sifai kuinama, nimfungulie kanda za viatu vyake. Mimi nimewabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho takatifu. Ikawa siku zile, Yesu akaja toka Nasareti wa Galilea, akabatizwa na Yohana mle Yordani. Papo hapo alipotoka majini akaona, mbingu zikipasuka, akamwona Roho, anavyomshukia kama njiwa. Sauti ikatoka mbinguni: Wewe ndiwe mwanangu mpendwa, nimependezwa na wewe. Papo hapo Roho akamchukua, akampeleka nyikani. Akawa huko nyikani siku 40 akijaribiwa na Satani, tena wenzake walikuwa nyama wa porini. Kisha malaika wakamtumikia. Yohana alipokwisha fungwa, Yesu akaja Galilea, akautangaza Utume mwema wa Mungu, akasema: Siku zimetimia, nao ufalme wa Mungu umekaribia. Juteni, mwutegemee Utume mwema! Naye alipokuwa akitembea kandokando ya bahari ya Galilea, akamwona Simoni na Anderea, nduguye Simoni, wakitupa nyavu zao baharini, kwani walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia: Njoni, mnifuate! Nami nitawafanya kuwa wavua watu. Papo hapo wakaziacha nyavu, wakamfuata. Alipoendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo, mwana wa Zebedeo, na Yohana nduguye; nao walikuwa chomboni wakizitengeneza nyavu. Mara akawaita, nao wakamwacha baba yao Zebedeo mle chomboni pamoja na wafanya kazi, wakaja, wakamfuata nyuma yake. Wakaenda, wakaingia Kapernaumu. Ilipokuwa siku ya mapumziko, akaiingia nyumba ya kuombea, akafundisha. Wakashangazwa na mafundisho yake; kwani alikuwa akiwafundisha kama mwenye nguvu, si kama waandishi. Humo nyumbani mwao mwa kuombea mkawa na mtu aliyekuwa na pepo mchafu; akapaza sauti akisema: Tuko na jambo gani sisi na wewe, Yesu wa Nasareti? Umekuja kutuangamiza. Nakujua, kama u nani; ndiwe Mtakatifu wa Mungu. Yesu alipomkaripia akisema: Nyamaza, umtoke! ndipo, yule pepo mchafu alipomsukumasukuma, akalia kwa sauti kuu, kisha akamtoka. Wote wakaingiwa na kituko, hata wakaulizana wao kwa wao wakisema: Hilo ni jambo gani? Ni ufundisho mpya wa kinguvu. Anawaagiza hata pepo wachafu, nao humtii. Huo uvumi wake ukatoka, ukaenea upesi po pote katika nchi zote zilizozunguka Galilea. Hapo walipotoka nyumbani mwa kuombea wakaingia pamoja na Yakobo na Yohana nyumbani mwao Simoni na Anderea. Naye mama ya mkewe Simoni alikuwa amelala kwa kuwa na homa. Papo hapo, walipomwambia, alivyokuwa, akamjia, akamwinua na kumshika mkono; ndipo, homa ilipomwacha, akawatumikia. Ilipokuwa jioni, jua lilipokwisha kuchwa, wakampelekea wote waliokuwa hawawezi, nao waliopagawa na pepo, mji wote ukawa umekusanyika mlangoni. Akawaponya wengi waliokuwa hawawezi, wenye magonjwa mengi, akafukuza pepo wengi akiwakataza pepo kusema, ya kuwa walimjua. Asubuhi na mapema sana akainuka, akatoka, akaenda zake mahali palipokuwa pasipo watu; hapo ndipo, alipomwomba Mungu. Naye Simoni na wenziwe wakamfuata mbio; walipomwona wakamwambia: Wote wanakutafuta. Akawaambia: Twendeni pengine penye vijiji vya pembenipembeni, nipate kupiga mbiu humo namo! Kwani hiyo ndiyo, niliyojia. Akaenda katika nchi yote ya Galilea, akapiga mbiu katika nyumba zao za kuombea, akafukuza pepo. Mwenye ukoma akaja kwake, akambembeleza na kumpigia magoti akimwambia: Ukitaka waweza kunitakasa. Ndipo, alipomwonea uchungu, akanyosha mkono, akamgusa, akamwambia: Nataka, utakaswe. Mara ukoma ukamwondoka, akatakaswa. Papo hapo akamkimbiza na kumkemea akimwambia: Tazama, usimwambie mtu neno! Ila uende zako, ujionyeshe kwa mtambikaji, uvitoe vipaji kwa ajili ya kutakaswa kwako, Mose alivyoviagiza, vije vinishuhudie kwao! Lakini alipotoka akaanza kutangaza mengi na kulisimulia jambo hilo po pote. Kwa hiyo Yesu hakuweza tena kuingia mjini waziwazi, ila alikuwa akikaa nje mahali palipokuwa pasipo watu, lakini watu wakamwendea toka pande zote. Siku zilipopita, akaingia tena Kapernaumu. Watu waliposikia, ya kuwa yumo nyumbani, wakakusanyika wengi, wasienee mle nyumbani, wala mlangoni, akawaambia lile Neno. Kukaja watu waliomletea mgonjwa wa kupooza, akichukuliwa na watu wanne; wasipoweza kumpelekea yeye kwa ajili ya watu wengi wakafumua paa hapo, alipokuwapo. Walipokwisha kupatoboa wakakishusha kitanda, alichokilalia yule mgonjwa wa kupooza. Yesu alipoona, walivyomtegemea, akamwambia mwenye kupooza: Mwanangu, makosa yako yameondolewa. Mlikuwamo na waandishi waliokaa mlemle, wakawaza mioyoni mwao ya kwamba: Haya huyu anayasemaje? Anambeza Mungu Yuko nani awezaye kuondoa makosa? Siye Mungu peke yake? Kwa kutambua rohoni mwake, ya kuwa wanawaza hivyo mioyoni mwao, Yesu akawaambia: Mbona mnawaza hivyo mioyoni mwenu? Kilicho chepesi ni kipi? Kumwambia mwenye kupooza: Makosa yako yameondolewa! au kusema: Inuka, ukichukue kitanda chako, uende? Lakini kusudi mpate kujua, ya kuwa Mwana wa mtu ana nguvu ya kuondoa makosa nchini, akamwambia mwenye kupooza: Nakuambia: Inuka, jitwishe kitanda chako, uende nyumbani kwako! Ndipo, alipoinuka, akajitwisha papo hapo kitanda, akatoka machoni pao wote. Kwa hiyo wote wakashangaa, wakamtukuza Mungu wakisema: Yaliyo kama hayo hatujayaona kamwe. Alipotoka tena kwenda kandokando ya bahari, kundi lote la watu likamjia, akawafundisha. Kisha alipokuwa akitembea akamwona Lawi, mwana wa Alfeo, amekaa forodhani. Akamwambia: Nifuata! Akainuka, akamfuata. Ikawa, alipokaa chakulani nyumbani mwake, ndipo, watoza kodi na wakosaji wengi walipokaa chakulani pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwani walikuwa wengi walipokaa chakulani pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwani walikuwa wengi waliomfuata. Waandishi wa Kifariseo walipomwona, ya kuwa anakula pamoja na wakosaji na watoza kodi, wakawaambia wanafunzi wake; Kumbe anakula pamoja na watoza kodi na wakosaji! Yesu alipoyasikia akawaambia: Walio wazima hawapaswi na mganga, ila walio wagonjwa. Sikujia kuwaita waongofu, ila wakosaji. Wanafunzi wa Yohana na Mafariseo walikuwa wakifunga. Wakaja, wakamwambia: Kwa nini wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafariseo hufunga, lakini wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia: Walioalikwa arusini hawawezi kufunga, bwana arusi akingali pamoja nao. Siku zote, wanapokuwa na bwana arusi, hawawezi kufunga. Lakini siku zitakuja, watakapoondolewa bwana arusi; siku ile ndipo, watakapofunga. Hakuna mtu anayetia kiraka cha nguo mpya katika kanzu chakavu; kama anafanya hivyo, kile kiraka kipya kinaondoa pote paliposhonwa katika kanzu chakavu; hivyo tundu lake litakuwa kubwa zaidi. Wala hakuna mtu anayetia mvinyo mpya katika viriba vichakavu; kwani akiitia mle, mvinyo itavipasua viriba, nayo mvinyo itaangamia pamoja na viriba. Ila mvinyo mpya hutiwa katika viriba vipya. Akawa akipita katika mashamba siku ya mapumziko; nao wanafunzi wake wakaanza kuendelea njiani wakikonyoa masuke. Lakini Mafariseo wakamwambia: Tazama! Mbona wanafanya siku ya mapumziko yaliyo mwiko? Naye akawaambia: Hamjasoma bado, Dawidi alivyofanya alipokosa chakula, wakaona njaa yeye na wenziwe? Hapo aliingia Nyumbani mwa Mungu kwa mtambikaji mkuu Abiatari, akaila mikate aliyowekewa Bwana, nayo kuila ni mwiko, huliwa na watambikaji tu; kisha akawapa nao wenziwe waliokuwa naye. Akawaambia: Siku ya mapumziko iliwekwa kwa ajili ya mtu; lakini mtu hakuwekwa kwa ajili ya siku ya mapumziko. Kwa hiyo Mwana wa mtu ni bwana hata wa siku ya mapumziko. Alipoingia tena katika nyumba ya kuombea, mle mlikuwa na mtu mwenye mkono uliokuwa umekaukiana. Wakamtunduia, kama atamponya siku ya mapumziko, wapate kumsuta. Akamwambia yule mwenye mkono uliokaukiana: Inuka, uje hapa katikati! Kisha akawauliza: Iko ruhusa siku ya mapumziko kufanya mema au kufanya maovu? kuponya roho ya mtu au kuiua? Waliponyamaza, ukali ukamjia, akawatazama waliokuwako, akausikitikia ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu: Unyoshe mkono wako! Alipounyosha, huo mkono wake ukageuka kuwa mzima. Mafariseo wakatoka, papo hapo wao pamoja na watu wa Herode wakamlia njama ya kumwangamiza. Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake kwenda upande wa baharini. Kundi la watu wengi sana waliotoka Galilea likamfuata. Tena wengi waliotoka Yudea na Yerusalemu na Idumea na ng'ambo ya Yordani na upande wa Tiro na Sidoni, wakamwendea, kwani waliyasikia yote, aliyoyafanya. Akawaambia wanafunzi wake, wamtengenezee chombo kidogo kwa ajili ya makundi ya watu, wasije kumsongasonga. Kwa kuwa aliponya wengi, wote walioteseka wakamwangukiaangukia, wapate kumgusa tu. Hata pepo wachafu, kila walipomwona, wakamwangukia wakipiga kelele wakisema: Wewe ndiwe Mwana wa Mungu! Akawatisha sana, wasimtangaze. Kisha akapanda mlimani, akawaita, aliowataka mwenyewe; wakaja kwake. Akawaweka kumi na wawili, wawe pamoja naye, apate kuwatuma kupiga mbiu, wakiisha kupewa nguvu za kufukuza pepo. Akawaweka hao kumi na wawili: Simoni akampa jina la Petero. Yakobo, mwana wa Zebedeo, na Yohana, nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge, ni kwamba: Wana wa Ngurumo. Akawaweka nao akina Anderea na Filipo na Bartolomeo na Mateo na Toma na Yakobo, mwana wa Alfeo, na Tadeo na Simoni wa Kana na Yuda Iskariota aliyemchongea halafu. Alipoingia nyumbani, ndipo, kundi la watu lilipokusanyika tena, wenyewe wasiweze hata kula mkate. Lakini ndugu zake walipoyasikia wakatoka, waje kumchukua, kwa maana walisema: Amepatwa na kichaa. Nao waandishi waliokuwa wametelemka toka Yerusalemu walisema: Ana Belzebuli. Tena wakasema: Nguvu ya huyo mkuu wa pepo ndiyo, anayofukuzia pepo. Akawaita, akawaambia kwa mifano: Satani awezaje kumfukuza Satani mwenziwe? Ufalme unapogombana wao kwa wao, ufalme huo hausimamiki. Nayo nyumba inapogombana wao kwa wao, nyumba hiyo haitaweza kusimama. Naye Satani anapojiinukia mwenyewe na kujigombanisha hawezi kusimama, ila ataishiwa. Hakuna mtu awezaye kuingia katika nyumba ya mwenye nguvu, aviteke vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; kisha ataweza kuiteka nyumba yake. Kweli nawaambiani: Wana wa watu wataondolewa yote, hata maneno yote ya kumbeza Mungu. Lakini mtu atakayembeza Roho Mtakatifu hapati kuondolewa kale na kale, ila kosa lake litamkalia pasipo mwisho. Aliwaambia hivyo kwa vile walivyosema: Ana pepo mchafu. Kisha mama yake na ndugu zake wakaja, wakasimama nje, wakatuma mtu kwake, amwite. Kundi la watu likawamo likimzunguka, wakamwambia: Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta. Akajibu akiwaambia: Aliye mama yangu ni nani? Ndugu zangu ni akina nani? Akawatazama waliokaa huko na huko, wakimzunguka pande zote, akasema: Watazameni walio mama yangu na ndugu zangu! Mtu ye yote atakayeyafanya, Mungu ayatakayo, huyo ndiye ndugu yangu na dada yangu na mama yangu. Akaanza tena kufundisha kandokando ya bahari. Wakamkusanyikia kundi la watu wengi mno; kwa hiyo akaingia chomboni, akakaa ufukoni, watu wote wakiwa pwani kandokando ya bahari. Akawafundisha maneno mengi kwa mifano, akawaambia katika mafunzo yake: Sikilizeni! Tazameni, mpanzi alitoka kumiaga mbegu. Ikawa, alipozimiaga, nyingine zikaangukia njiani; ndege wakaja, wakazila. Nyingine zikaangukia penye miamba pasipo na udongo mwingi. Kuota zikaota upesi kwa kuwa na udongo kidogo, lakini jua lilipokuwa kali, zikanyauka, kwa kuwa hazina mizizi. Nyingine zikaangukia penye miiba; nayo miiba ilipoota ikazisonga, zisizae. Nyingine zikaangukia penye mchanga mzuri, zikazaa zikikua na nguvu, zikatoa kama punje thelathini, hata sitini, hata mia. Akasema: Mwenye masikio yanayosikia na asikie! Naye alipokuwa peke yake, wafuasi wake pamoja na wale kumi na wawili wakamwuliza maana ya mifano. Akawaambia: Ninyi mmepewa kulitambua fumbo la ufalme wa Mungu, lakini wale walioko nje huambiwa hayo yote kwa mifano, kusudi watazame, lakini wasione, wasikilize, lakini wasijue maana, wasije wakanigeukia, wakaondolewa makosa. Akawaambia: Msipoujua mfano huu mtaitambuaje mifano yote? Mwenye kumiaga analimiaga Neno. Lakini zilizoko njiani ndio hao: Neno linapomiagwa, wakiisha kulisikia, papo hapo Satani huja, akaliondoa Neno lililomiagwa mwao. Vilevile zilizomiagwa penye miamba ndio hao: wanapolisikia Neno, papo hapo hulipokea kwa furaha, lakini hawana mizizi mioyoni mwao, ila wanalishika kwa kitambo kidogo tu. Yanapotukia maumivu au mafukuzo kwa ajili ya Neno, mara hujikwaa. Nyingine ndizo zilizomiagwa penye miiba, ndio hao: wanalisikia Neno, lakini masumbuko ya dunia hii na udanganyifu wa mali na tamaa nyingine zikiwaingia hulisonga Neno, lisizae matunda. Nazo zile zilizomiagwa penye mchanga mzuri ndio hao: wanalisikia Neno na kulipokea, kisha huzaa matunda, kama thelathini, hata sitini, hata mia. Akawauliza: Iko taa inayoletwa, iwekwe chini ya kapu au mvunguni mwa kitanda? Hailetwi, iwekwe juu ya mwango? Kwani hakuna lililofichwa, isipokuwa kwamba lipate kufunuliwa halafu; wala hakuna njama, ila kwamba ipate kutokea waziwazi. Mtu akiwa na masikio yanayosikia na asikie! Akawaambia: Mwangalie, jinsi mnavyosikia! Kipimo, mnachokipimia wengine, ndicho, mtakachopimiwa nanyi, tena mtaongezewa. Kwani aliye na mali atapewa; lakini asiye na kitu atachukuliwa hata kile, alicho nacho. *Akasema: Ufalme wa Mungu unakuwa hivyo, kama mtu anayemiaga mbegu katika nchi. Kisha hulala na kuamka usiku na mchana, nazo mbegu humea na kukua, yeye asivijue, vilivyo. Nchi huzaa yenyewe kwanza hutoa mimea, halafu suke, halafu ngano zinazojaa katika suke. Lakini punje zinapopevuka, mwenyewe mara hutuma wenye miundu, kwani mavuno yamefika.* Akasema: Ufalme wa Mungu tuufananishe na nini? Au tuueleze kwa mfano gani? Umefanana na kipunje cha haradali. Kinapopandwa katika nchi ni kidogo kuliko mbegu zote zilizoko huku nchini. Tena kikiisha pandwa hukua, kiwe mkubwa kuliko miboga yote kwa kuchipuza matawi makubwa, hata ndege wa angani huweza kuja na kutua katika kivuli chake. Kwa mifano mingi inayofanana na huu akawaambia Neno, kama walivyoweza kusikia; lakini pasipo mfano hakuwaambia neno. Lakini wanafunzi wake akawafungulia yote, walipokuwa peke yao. Siku ile ilipokuwa jioni, akawaambia: Tuvuke kwenda ng'ambo! Wakaliacha kundi la watu, wakamchukua hivyo alivyokuwa chomboni; navyo vyombo vingine vilikuwa pamoja naye. Kukawa na msukosuko mkubwa wa upepo, mawimbi yakakipigapiga chombo, hata chombo kikawa kinajaa maji. Naye alikuwa chomboni upande wa nyuma, amelala usingizi juu ya mto. Ndipo, walipomwamsha wakimwambia: Mfunzi, huoni uchungu, tukiangamia? Akainuka, akaukaripia upepo, akaiambia bahari: Nyamaza, utulie! Papo haupepo ukakoma, kukawa kimya kabisa. Kisha akawaambia: Mbona mnaogopa hivyo? Mbona hamnitegemei? Wakaingiwa na woga mkubwa, wakasemezana wao kwa wao: Ni mtu gani huyu, ya kuwa hata upepo na bahari zinamtii? Wakafika ng'ambo ya bahari katika nchi ya Wagerasi. Alipotoka chomboni papo hapo akakutana na mtu mwenye pepo mchafu aliyetoka penye makaburi. Kwa kuwa hukaa pale penye makaburi, hakuwako mtu aliyeweza kumfunga kwa mnyororo wo wote. Kwani alikuwa amefungwa mara nyingi kwa mapingu na kwa minyororo, lakini minyororo ikararuliwa naye, nayo mapingu yakasagwa naye, mpaka yakikatika, kwa hiyo hakukuwako kabisa mtu mwenye nguvu za kumshinda. Siku zote mchana kutwa alikuwa penye makaburi nako milimani akipiga makelele na kujipigapiga mawe mwenyewe. Alipomwona Yesu, yuko mbali bado, akapiga mbio, akaja, akamwangukia, akapaza sana sauti akisema: Tuko na jambo gani mimi na wewe Yesu, Mwana wa Mungu Alioko huko juu? Nakuapisha kwa Mungu, usiniumize! Kwani alikuwa amemwambia: Wee pepo mchafu, umtoke mtu huyu! Alipomwuliza: Jina lako nani? akamwambia: Jina langu mimi Maelfu, kwa kuwa tumo wengi. Akambembeleza sana, asiwafukuze, waitoke nchi ile. Basi, kulikuwako kule mlimani kundi kubwa la nguruwe waliokuwako malishoni. Wakambembeleza wakisema: Tutume kwenda kwao wale nguruwe, tupate kuwaingia! Alipowapa ruhusa, pepo wachafu wakamtoka, wakawaingia nguruwe; ndipo, kundi lilipotelemka mbio mwambani, wakaingia baharini, wapata kama 2000, wakatoswa baharini. Lakini wachungaji wao wakakimbia, wakayatangaza mjini na mashambani. Watu wakaja, watazame, lililofanyika lilivyo. Walipofika kwa Yesu na kumtazama yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu wa Maelfu, anavyokaa amevaa nguo, tena ana akili zake, wakashikwa na woga. Nao walioyaona wakawasimulia, ya mwenye pepo yalivyoendelea, hata yale ya nguruwe. Wakaanza kumbembeleza, atoke mipakani kwao. Alipojipakia chomboni, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akambembeleza, afuatane pamoja naye. Lakini hakumwitikia, ila akamwambia: Uende zako nyumbani mwako kwa ndugu zako ukawasimulie yote, Bwana aliyokutendea kwa kukuhurumia! Ndipo, alipokwenda zake, akaanza kuyatangaza katika ile Miji Kumi yote, Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu. Yesu alipokwisha vuka tena chomboni kuja ng'ambo, kundi la watu wengi likakusanyika hapo, alipokuwa kandokando ya bahari. Akaja mmoja wao majumbe wa nyumba ya kuombea, jina lake Yairo; alipomwona akamwangukia miguuni pake, akambembeleza sana akisema: Kibinti changu yumo kufani; nakuomba, uje, umbandikie mikono, apate kupona na kuwa mzima tena. Akaondoka, akaenda naye; watu wengi sana wakamfuata wakimsongasonga. Kukawa na mwanamke mwenye ugonjwa wa kutoka damu miaka 12. Huyo alikuwa amepata maumivu mengi kwa waganga wengi; hivyo alizimaliza mali zake zote, lakini hawakumfaa hata kidogo, ugonjwa wake ukakaza tu kuwa mbaya. Alipoyasikia mambo ya Yesu akaliingia kundi la watu, akamjia nyuma, akaigusa nguo yake. Maana alisema: Hata nikizigusa nguo zake tu nitapona. Papo hapo kijitojito cha damu yake kikakauka, akajiona mwilini, ya kuwa amelipona teso lake. Papo hapo Yesu akatambua mwilini mwake, ya kuwa nguvu imemtoka; akaligeukia kundi la watu, akasema: Yuko nani aliyenigusa nguo zangu? Wanafunzi wake wakamwambia: Unaliona kundi la watu, linakusongasonga, nawe unauliza: Yuko nani aliyenigusa? Alipotazama huko na huko, apate kumwona aliyemgusa, yule mwanamke akashikwa na woga, akatetemeka, kwani alijua lililompata; kwa hiyo akaja, akamwangukia, akamwambia yote, yalivyokuwa kweli. Naye akamwambia: Mwanangu, kunitegemea kwako kumekuponya, nenda na kutengemana, uwe mzima, teso lako lisikurudie tena! Angali akisema, wakaja watu wa jumbe wa nyumba ya kuombea, wakasema: Binti yako amekwisha kufa; mfunzi unamsumbulia nini tena? Yesu alipoyasikia maneno haya, yakisemwa, akamwambia jumbe wa nyumba ya kuombea: Usiogope, nitegemea tu! kisha hakumpa mtu mwingine ruhusa kufuatana naye, ila Petero na Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo. Walipoingia nyumbani mwa jumbe wa nyumba ya kuombea, akaona makelele ya watu, wakilia na kuomboleza sana. Akaingia, akawaambia: Mnapigia nini makelele na kulia? Kitoto hakufa, ila amelala usingizi tu; ndipo, walipomcheka sana. Lakini alipokwisha kuwafukuza wote akamchukua baba ya kitoto na mama yake na wale waliokuwa pamoja naye, akaingia mle, yule kitoto alimokuwa. Akamshika kitoto mkono, akamwambia: Talita kumi! ni kwamba: Kijana, nakuambia: Inuka! Papo hapo kijana akafufuka, akaendaenda, kwani alikuwa wa miaka 12. Ndipo, waliposhangaa ushangao mwingi. Akawakataza sana, wasilitambulishe neno hili kwa mtu ye yote; kisha akasema, kijana apewe chakula. Akatoka kule, akaenda kwao, alikokulia, nao wanafunzi wake wakamfuata. Ilipokuwa siku ya mapumziko, akaanza kufundisha katika nyumba ya kuombea, nao wengi waliomsikia wakashangaa, wakasema: Huyu haya ameyapata wapi? Werevu huu ulio wa kweli amepewa na nani? Hizo nguvu nazo zinazotendwa na mikono yake ni nguvu gani? Huyu si seremala, mwana wa Maria? Huyu si ndugu yao Yakobo na Yose na Yuda na Simoni? Nao maumbu zake hawako huku kwetu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia: Mfumbuaji habezwi, isipokuwa kwao, alikokulia, na kwa ndugu zake namo nyumbani mwake. Kwa hiyo hakuweza kufanya kule la nguvu hata moja, ila wanyonge wachache akawabandikia mikono, akawaponya. Akastaajabu, jinsi walivyokataa kumtegemea. Akaenda akizunguka katika vijiji vya pembenipembeni na kufundisha watu. Akawaita wale kumi na wawili, akaanza kuwatuma wawiliwawili, akawapa nguvu za kufukuza pepo wachafu. Akawaagiza, washike fimbo tu, wasichukue kingine cha njiani, wala chakula wala mkoba wala senti mishipini. Mwende mmevaa viatu, lakini msivae nguo mbili! Akawaambia: Kila mtakamoingia nyumbani, kaeni mwake, mpaka mtakapotoka tena! Napo mahali, wasipowapokea, wasiwasikilize, basi, tokeni pale na kuyakung'uta mavumbi yaliyoishika miguu yenu, yaje yanishuhudie kwao! Kisha wakatoka, wakaenda na kutangaza, watu wajute. Wakafukuza pepo wengi, wakapaka wanyonge wengi mafuta, wakawaponya. Mfalme Herode akayasikia, kwani Jina lake lilivuma, maana watu walisema: Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, kwa sababu hii nguvu hizo humtendesha kazi. Lakini wengine walisema: Ndiye Elia; wengine tena walisema: Ni mfumbuaji kama wale wafumbuaji wenzake. Lakini Herode alipoyasikia akasema: Ndiye Yohana, niliyemkata kichwa mimi, huyo amefufuka. Kwani Herode mwenyewe alikuwa ametuma kumkamata Yohana na kumfunga kifungoni kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, Filipo, ambaye alikuwa amemwoa. Kwani Yohana alimwambia Herode: Ni mwiko kwako kuwa na mke wa nduguyo. Lakini Herodia alimvizia, akataka kumwua, asiweze. Kwani Herode alimwogopa Yohana, kwa vile, alivyomjua kuwa mtu mwongofu na mtakatifu, akamshika na kumlinda. Naye alipomsikia mara kwa mara akahangaishwa sana moyoni, tena akapendezwa kumsikiliza. Siku iliyofaa ya kumpata ilikuwa sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode; ndipo, alipowaalika chakulani watawala miji yake na wakubwa wa askari na watu wenye cheo wa Galilea. Binti Herodia alipoingia na kucheza ngoma, akampendeza Herode na wale waliokaa pamoja naye chakulani. Ndipo, mfalme alipomwambia huyo msichana: Niombe kila, utakacho! nitakupa; kisha akamwapia: Cho chote, utakachoniomba, nitakupa, ijapo iwe nusu ya ufalme wangu. Yule akatoka, akamwuliza mama yake: Niombe nini? Naye akasema: Kichwa chake Yohana Mbatizaji! Papo hapo akaingia mbio kwa mfalme, akaomba akisema: Nataka, unipe sasa hivi katika chano kichwa chake Yohana Mbatizaji. Mfalme akasikitika sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake na kwa ajili ya wale waliokaa chakulani hakutaka kumnyima. Ndipo, mfalme alipotuma askari, akamwagiza, akilete kile kichwa chake. Yule akaenda, akamkata kichwa chake mle kifungoni, kisha akakileta katika chano, akampa msichana, naye msichana akampa mama yake. Wanafunzi wake walipoyasikia wakaja, wakautwaa mwili wake, wakauweka kaburini. Nao mitume wakakusanyika kwa Yesu, wakamsimulia mambo yote, waliyoyafanya nayo waliyoyafundisha. Akawaambia: Njoni ninyi peke yenu, twende mahali pasipo na watu, mpumzike kidogo! Kwani watu wengi walikuwa wakija, tena wakienda, wasipate hata kula. Wakaondoka, wakaenda chomboni peke yao mahali palipokuwa pasipo watu. Watu walipowaona, wakitoka, nao wengi walipotambua, wanapokwenda, wakatoka miji yote kwa miguu, wakapiga mbio kuwakuta palepale, wakatangulia kufika. Alipotoka chomboni akaona, watu ni wengi sana, akawaonea uchungu, kwani walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji, akaanza kuwafundisha mengi. Saa zilipofika za jioni, wanafunzi wake wakamjia, wakasema: Hapa tulipo ni nyika, nazo saa zimefika za jioni. Uwaage watu, waende zao mashambani na vijijini huko pembenipembeni, wajinunulie vyakula! Lakini akawajibu akiwaambia: Wapeni ninyi vyakula! Wakamwambia: Twende, tununue mikate ya shilingi 200, tuwape, wale? Akawauliza: Mnayo mikate mingapi? Haya! Nendeni, mtazame! Walipoijua wakasema: Mitano, tena visamaki viwili. Akawaagiza wote, wakae mafungumafungu uwandani penye majani. Wakakaa kikao kwa kikao, pengine mia, pengine hamsini. Akaitwaa ile mikate mitano na vile visamaki viwili, akatazama juu mbinguni, akaviombea, akawamegeamegea ile mikate, akawapa wanafunzi, wawapangie; navyo vile visamaki viwili akawagawia wote. Wakala wote, wakashiba. Kisha wakaokota makombo ya mikate wakajaza vikapu kumi na viwili pamoja na vipande vya samaki. Nao waliokula ile mikate walikuwa 5000 waume tu. Papo hapo akawashurutisha wanafunzi wake, waingie chomboni, wamtangulie kwenda ng'ambo huko Beti-Saida, mpaka yeye kwanza aliage kundi la watu. Naye alipokwisha kuwaaga akaondoka kwenda mlimani kuomba. Jua lilipokwisha kuchwa, chombo kilikuwa katikati ya bahari, naye mwenyewe alikuwa peke yake pwani. Akawaona, wakihangaishwa, wasiweze kwendelea, kwani upepo uliwatokea mbele. Ilipofika zamu ya nne ya usiku, akawajia akienda juu ya bahari, akataka kuwapita. Nao walipomwona, anavyokwenda juu ya bahari, wakawaza kuwa ni mzimu, wakapiga makelele, kwani wote walimwona, wakatetemeka. Papo hapo yeye akasema nao akawaambia: Tulieni! Ni miye, msiogope! Alipowapandia chomboni, upepo ukakoma. Ndipo, walipostuka na kushangaa mno mioyoni mwao; kwani hawajaelewa maana ya ile mikate, mioyo yao nayo ilikuwa imeshupaa. Walipokwisha vuka wakafika nchini kwa Genesareti, wakatia nanga hapo. Nao walipotoka chomboni, papo hapo watu wakamtambua; wakaenda mbio wakiizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani waliokuwa hawawezi, wakaenda nao huko na huko, walikomsikia, ya kuwa yeye yuko. Kila alipoingia katika vijiji au miji au mashamba waliwaweka wagonjwa sokoni, wakambembeleza, wamguse pindo la lanzu yake tu; nao wote walioligusa wakapona. Wakamkusanyikia Mafariseo na wengine waliokuwa waandishi waliotoka Yerusalemu. Wakaona wanafunzi wake, wanavyokula vyakula kwa mikono hivyo ilivyo, maana haikunawiwa. Kwani Mafariseo na Wayuda wote hawali, wasiponawa mikono na kuikamua; huku ni kuyashika mazoezo ya wakale. Navyo vya sokoni hawavili, wasipoviosha kwanza; nayo mambo mengine mengi yako, waliyoyapokea kuyashika, kama kuosha vinyweo na mitungi na vyungu na vitanda. Mafariseo na waandishi walipomwuliza: Kwa sababu gani wanafunzi wako hawaendi na kuyafuata mazoezo ya wakale, ila hula chakula kwa mikono hivyo ilivyo? akawaambia: Yesaya aliyafumbua vizuri hayo mambo yenu, ninyi wajanja, kama yalivyoandikwa kwamba: Ukoo huu huniheshimu kwa midomo tu, lakini mioyo yao inanikalia mbali. Hivyo hunicha bure, kwani hufundisha mafundisho yaliyo maagizo ya watu tu. Mnaliacha agizo lake Mungu, myashike mazoezo ya watu. Akawaambia: Vizuri vyenu ni kulitengua agizo lake Mungu, mpate kuyaangalia mazoezo ya wakale wenu. Kwani Mose alisema: Mheshimu baba yako na mama yako! na tena: Atakayemwapiza baba au mama sharti afe kwa kuuawa! Lakini ninyi husema: Mtu akimwambia baba au mama: Korbani, ni kwamba: Mali, unazozitaka, nikusaidie nazo, amepewa Mungu, basi, ni vema. Hivyo mnamzuia mtu huyo, asimpatie baba wala mama kitu; hivyo mnalitangua Neno la Mungu kwa ajili ya mazoezo, mliyozoezwa na wakale wenu. Tena mnafanya mengi yanayofanana na hayo. Akaliita tena kundi la watu, akawaambia: Nisikilizeni nyote, mjue maana! Hakuna kitu kilichoko nje ya mtu kinachoweza kumtia uchafu kikiingia ndani yake; ila yanayomtoka mtu ndiyo yanayomtia uchafu. Kama yuko mwenye masikio yanayosikia na asikie! Kisha alipoondoka penye watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza mfano ule. Akawaambia: Kumbe nanyi hamjaerevuka hata leo! Hamjui, kila kitu kilichoko nje kikiingia ndani ya mtu hakiwezi kumtia uchafu? Kwa kuwa hakimwingii moyoni, ila tumboni tu, kikatoka chooni; ndivyo, alivyotengua miiko yote ya vyakula. Akasema: Linalomtoka mtu hilo ndilo linalomtia mtu uchafu. Kwani ndani mioyoni mwa watu hutoka mawazo mabaya: ugoni, wizi, uuaji, uzinzi, choyo, ubaya, unyengaji, uasherati, kijicho, matusi, majivuno, upuzi. Mabaya haya yote hutoka ndani, tena ndiyo yanayomtia mtu uchafu. Alipoondoka pale, akaenda mipakani kwa Tiro, akaingia nyumbani, maana alitaka, asijulikane na mtu, lakini hakuweza kufichika. Kwani papo hapo mwanamke alisikia, ya kuwa yuko. Kwa kuwa na mtoto mwenye pepo mchafu akaja, akamwangukia miguuni pake; naye yule mwanamke alikuwa Mgriki, kabila lake ni Msirofoniki. Alipomwomba, amfukuze pepo, amtoke binti yake, akamwambia: Uache, kwanza watoto washibe, kwani haifai kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia vijibwa! Lakini akamjibu akisema: Ndio, Bwana, lakini nao vijibwa hula chini ya meza makombo ya vitoto. Ndipo, alipomwambia: Kwa ajili ya neno hili enenda, pepo amemtoka binti yako! Akaondoka, akaenda nyumbani mwake, akamkuta kitoto, amelala kitandani, naye pepo alikuwa amekwisha kumtoka. *Alipotoka tena mipakani kwa Tiro akapita Sidoni, akafika kwenye bahari ya Galilea katikati ya mipaka ya ile Miji Kumi. Wakamletea mtu aliyekuwa kiziwi na bubu, wakambembeleza, ambandikie mkono. Akamwondoa katika kundi la watu, wawe peke yao, akaweka vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi. Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia: Efata! ni kwamba: Fumbuka! Ndipo, masikio yake yalipofumbuka, nayo mafungo ya ulimi wake yakalegea papo hapo, akasema vema. Akawaagiza, wasimwambie mtu. Lakini ijapo awaagize hivyo, wale walizidi kuyatangaza po pote. Watu wakashangaa mno, wakasema: Ametenda vyote vizuri; viziwi anawafanya, wasikie, nao mabubu, waseme.* Siku zile likakusanyika tena kundi la watu wengi; walipokosa vyakula, akawaita wanafunzi, akawaambia: Kundi hili la watu nalionea uchungu, kwa kuwa wameshinda kwangu siku tatu, wasione chakula. Kama ninawaaga, waende nyumbani kwao pasipo kula, watazimia njiani; tena wako waliotoka mbali. Wanafunzi wake walipomjibu: Hapa nyikani mtu atawezaje kuwashibisha watu hawa mikate? akawauliza: Mnayo mikate mingapi? Nao waliposema: Saba, akawaagiza hao watu wengi, wakae chini, kisha akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake, wawapangie; nao wakawapangia wao wa hilo kundi la watu. Tena walikuwa na visamaki vichache; navyo akaviombea, akasema, wawapangie hivi navyo. Wakala, wakashiba; kisha wakaokota makombo ya mikate yaliyosalia, yakawa makanda saba. Nao walikuwa kama 4000. Kisha akawaaga, waende zao. Papo hapo akaingia chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaja upande wa Dalmanuta. Wakamtokea Mafariseo, wakanza kubisha naye, wakamjaribu wakitaka, afanye kielekezo kitokacho mbinguni. Akapiga kite rohoni mwake, akasema: Mbona wao wa ukoo huu wanataka kielekezo? Kweli nawaambiani: Wao wa ukoo huu hawatapata kielekezo. Kisha akawaacha, akajipakia tena chomboni, akaenda zake ng'ambo. Walikuwa wamesahau kuchukua mikate; namo chomboni hawakuwa na mikate ila mmoja tu. Akawaonya akisema: Tazameni, jiangalieni kwa ajili ya chachu ya Mafariseo na chachu ya Herode! Ndipo, walipoyafikiri na kusemezana wao kwa wao: Ni kwa sababu hatunayo mikate. Kwa kuwatambua akawaambia: Mbona mnafikiri hivyo, ya kuwa hamnayo mikate? Hamjaerevuka bado? Wala hamjajua maana? Mngaliko wenye mioyo iliyoshupaa? Macho mnayo, lakini hamwoni? Nayo masikio mnayo, lakini hamsikii? Wala hamwikumbuki ile mikate mitano, nilipoimegea wale 5000? Hapo mlijaza makapo mangapi mkiokota makombo? Wakamwambia: Kumi na mawili. Wala hamwikumbuki ile mikate saba, nilipoivunjia wale 4000, mlijaza makanda mangapi mkiokota makombo? Wakamwambia: Saba. Akawauliza: Hamjajua bado maana? Walipoingia Beti-Saida, wakamletea kipofu, wakambembeleza, amguse. Akaushika mkono wa kipofu, akamwongoza, watoke kijijini, akamtemea mate machoni, akambandikia mikono, akamwuliza: Kiko, unachokiona? Yule akainua macho, akasema: Naona watu wanaotembea, wanaonekana kuwa kama miti. Hapo akambandikia mikono tena machoni pake, akamwagiza kutazama tena; ndipo, macho yake yaliporudia kuwa mazima, akaona vitu vyote waziwazi, hata vilivyoko mbali. Kisha akamtuma, aende nyumbani mwake, akisema: Kijijini usimwingie! Wala usimwambie mtu wa humu kijijini! Yesu na wanafunzi wake wakatoka, waingie vijiji vya upande wa Kesaria-Filipi. Walipokuwa njiani, akawauliza wanafunzi wake akiwaambia: Watu hunisema kuwa ni nani? Nao wakamwambia wakisema: Wanakusema kuwa u Yohana Mbatizaji, wengine: Elia, wengine: Mmoja wao wafumbuaji. Kisha akawauliza: Lakini ninyi mnanisema kuwa ni nani? Petero akajibu akimwambia: Wewe ndiwe Kristo. Ndipo, alipowatisha, wasimwambie mtu hilo neno lake. Akaanza kuwafundisha, ya kuwa imempasa Mwana wa mtu kuteswa mengi na kukataliwa nao wazee na watambikaji wakuu na waandishi, mpaka auawe, kisha afufuke, siku tatu zitakapopita. Neno hili akalisema waziwazi. Ndipo, Petero alipomchukua pembeni, akaanza kumtisha. Naye akageuka nyuma, akawatazama wanafunzi wake, akamtisha Petero akisema: Niondokea hapa nyuma yangu, wewe Satani! Kwani wewe huyawazi mambo ya Kimungu, ila unayawaza ya kiwatu tu. Akaliita kundi la watu, limjie pamoja na wanafunzi wake, akawaambia: Mtu akitaka kunifuata mimi ajikataze mapenzi yake, ajitwishe nao msalaba wake, kisha anifuate! Maana mtu anayetaka kuiokoa roho yake ataiangamiza. Lakini mtu atakayeiangamiza roho yake kwa ajili yangu mimi na kwa ajili ya Utume mwema ataiokoa. Kwani mtu vinamfaa nini kuvichuma vya ulimwengu wote, roho yake ikiponzwa navyo? Kwani mtu atoe nini, aikomboe roho yake? Kwani mtu atakayenionea soni mimi na maneno yangu kwao wa kizazi hiki kilicho chenye ugoni na ukosaji, basi, naye Mwana wa mtu atamwonea soni huyo atakapokuja mwenye utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu. Akawaambia: Kweli nawaambiani: Miongoni mwao wanaosimama hapa wamo wengine, ambao hawatakuonja kufa, mpaka watakapouona ufalme wa Mungu, ukiisha kuja kwa nguvu. Baada ya siku sita Yesu akamchukua Petero na Yakobo na Yohana, akapanda pamoja nao peke yao pasipo watu wengine juu ya mlima mrefu. Huko akageuzwa sura yake machoni pao, nazo nguo zake zikawa nyeupe sana, zikamerimeta; nchini hakuna fundi anayeweza kuzing'aza hivyo. Wakatokewa na Elia pamoja na Mose, wakawa wakiongea na Yesu. Petero akasema akimwambia Yesu: Mfunzi mkuu, hapa ni pazuri kuwapo sisi, na tujenge vibanda vitatu, kimoja chako, na kimoja cha Mose, na kimoja cha Elia! Kwani hakujua, alilolisema, kwa maana waliingiwa na woga mkubwa. Kisha hapo pakawa na wingu, likawatia kivuli, sauti ikatoka winguni kwamba: Huyu ndiye mwanangu mpendwa, msikilizeni yeye! Mara walipotazama huko na huko, hakuna waliyemwona, asipokuwa Yesu peke yake pamoja nao. Walipokuwa wakishuka mlimani, akawakataza, wasimsimulie mtu ye yote, waliyoyaona, isipokuwa hapo, Mwana wa mtu atakapokwisha kufufuka katika wafu. Wakalishika neno hili wakiulizana wao kwa wao: Huko kufufuka katika wafu maana yake nini? Wakamwuliza wakisema: Waandishi husemaje: Sharti kwanza Elia aje? Akawaambia: Kweli, Elia anakuja kwanza, vyote avigeuze kuwa vipya. Kisha Mwana wa mtu ameandikiwaje, ya kuwa atateswa mengi na kubezwa? Lakini nawaambiani: Elia amekwisha kuja, wakamtendea yote, waliyoyataka, kama alivyoandikiwa. Walipokuja kwa wanafunzi wakaona kundi la watu wengi lililowazunguka, hata waandishi walikuwapo wakibishana nao. Papo hapo kundi lote lilipomwona yeye, wakastuka, wakamwendea mbio, wakamwamkia. Akawauliza: Mnabishana nini nao? Mmoja wao wale watu wengi akamjibu: Mfunzi, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo wa ububu. Napo pote anapomkamata anamsukumasukuma kwa nguvu, naye hutoka pofu na kukereza meno, kisha mwili wake hunyauka. Nami nikawaambia wanafunzi wako, wamfukuze huyo pepo, lakini hawakuweza. Naye akawajibu akisema: Enyi wa kizazi kisichomtegemea Mungu! Nitakuwapo nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni hapa, nilipo! Wakampeleka kwake; naye alipomwona, mara pepo akamkumba, akaanguka chini, akafingirika na kutoka pofu. Akamwuliza baba yake: Hivyo vimempata tangu lini? Akasema: Tangu utoto wake; mara nyingi humtupa motoni na majini, maana amwue. Lakini ukiweza kitu tusaidie ukituonea uchungu! Yesu akamwambia: Ukiweza kumtegemea Mungu! Yote huwezekana kwake anayemtegemea Mungu. Papo hapo baba wa kijana akapaza sauti akisema: Namtegemea Mungu; nisaidie, nisipomtegemea! Yesu alipoona, watu wengi wanavyomkusanyikia mbiombio, akamkaripia yule pepo mchafu akimwambia: Wee pepo uliye bubu na kiziwi, mimi nakuagiza, umtoke huyu, usimwingie tena! Ndipo, alipolia, akamsukumasukuma kwa nguvu, akamtoka; naye akawa kama mfu, hata wengi wakasema: Amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua; ndipo, aliposimama. Naye alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza walipokuwa peke yao: Mbona sisi hatukuweza kumfukuza huyo? Akawaambia: Pepo walio hivyo hawawezi kutoka, isipokuwa kwa nguvu ya kuomba na ya kufunga. Wakatoka kule, wakatembea huko katikati ya Galilea; naye hakutaka, mtu akivitambua. Kwani alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake na kuwaambia: Mwana wa mtu atatiwa mikononi mwa watu, nao watamwua; lakini akiisha kuuawa, siku zitakapopita tatu, atafufuka. Nao hawakulitambua neno hili, lakini wakaogopa kumwuliza. Wakafika Kapernaumu. Alipokuwa nyumbani akawauliza: Njiani mlibishana nini? Wakanyamaza; maana walikuwa wameshindana njiani wao kwa wao kwamba: Aliye mkuu ni nani? Akakaa, akawaita wale kumi na wawili, akawaambia: Mtu akitaka kuwa wa kwanza, sharti awafuate wenzake wote nyuma, awe mtumishi wao wote! Kisha akatwaa kitoto, akamsimamisha katikati yao, akamkumbatia, akawaambia: Mtu atakayepokea kitoto mmoja aliye kama huyu kwa Jina languhunipokea mimi. Tena mtu akinipokea mimi hanipokei mimi, ila humpokea yule aliyenituma. Yohana akamwambia: Mfunzi, tuliona mtu anayefukuza pepo kwa Jina lako, lakini hafuatani nasi; tukamzuia, kwani hakufuatana nasi. Yesu akasema: Msimzuie! Kwani hakuna mwenye kufanya cha nguvu kwa ajina langua atakayeweza kipunde kidogo kunisema vibaya. Kwani asiyetukataa yuko upande wetu. Kwani atakayewanywesha ninyi kinyweo cha maji tu, kwa sababu m wa Kristo, kweli nawaambiani Mshahara wake hautampotea kamwe. Lakini mtu atakayekwaza mmoja tu aliye mwenzao hawa wadogo wanaonitegemea, itamwia vizuri zaidi, akitundikwa shingoni pake jiwe kubwa la kusagia, kisha atumbukizwe baharini. Nawe, mkono wako ukikukwaza, uukate! Kuingia penye uzima mwenye kilema kutakufaa kuliko hapo, ukiwa mwenye mikono miwili, ukajiendea kuzimuni penye moto usiozimika. Hapo ndipo, mdudu mwenye kuwaumiza asipokufa, tena ndipo, pasipozimika moto. Nawe, mguu wako ukikukwaza, uukate! Kuingia penye uzima, ukiwa kiwete, kutakufaa kuliko hapo, ukiwa mwenye miguu miwili, ukatupwa shimoni mwa moto. Hapo ndipo, mdudu mwenye kuwaumiza asipokufa, tena ndipo pasipozimika moto. Nalo jicho lako likikukwaza, basi, ling'oe, ulitupe mbali! Kuuingia ufalme wa Mungu mwenye chongo kutakufaa kuliko hapo, ukiwa mwenye macho mawili ukatupwa shimoni mwa moto. Hapo ndipo, mdudu mwenye kuwaumiza asipokufa, tena ndipo, pasipozimika moto. Kwani chumvi ya kumkoleza mtu ye yote ni moto. Chumvi ni nzuri; lakini chumvi ikiwa imepotewa na ukolezi, mtaitia kitu gani, ipate kukolea tena? Mwe na chumvi mioyoni mwenu! Tena mwendeane kwa utengemano! Akaondoka huko, akaja mipakani kwa Yudea na ng'ambo ya Yordani. Walipomkusanyikia tena makundi ya watu, akawafundisha tena, kama alivyozoea. Mafariseo wakamjia, wakamwuliza, kama iko ruhusa, mwanamume amwache mkewe. Naye akajibu akiwaambia: Mose aliwaagiza nini? Nao wakasema: Mose alitupa ruhusa kuandika cheti cha kuachana, kisha kumwacha. Yesu akawaambia: Kwa ajili ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia agizo hilo. Lakini tokea hapo mwanzo wa viumbe aliwaumba mume na mke. Kwa sababu hii mtu atamwacha baba yake na mama yake, nao hao wawili watakuwa mwili mmoja. Kwa hiyo sio wawili tena, ila wamekuwa mwili mmoja tu. Basi, Mungu alichokiunga, mtu asikiungue! Nyumbani wanafunzi wakamwuliza tena kwa ajili ya neno hilo. Akawaambia: Mtu akimwacha mkewe na kuoa mwingine anazini naye. Naye mke akimwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini. *Wakamletea vitoto, awaguse. Lakini wanafunzi waliwatisha waliowaleta. Yesu alipoviona akachukizwa, akawaambia: Waacheni vitoto, waje kwangu, msiwazuie! Kwani walio hivyo ufalme wa Mungu ni wao. Kweli nawaambiani: Mtu asiyeupokea ufalme wa Mungu kama kitoto hatauingia kamwe. Kisha akawakumbatia, akawabariki akiwabandikia mikono.* *Alipotoka na kufika njiani, mmoja akamjia mbio, akampigia magoti, akamwuliza: Mfunzi mwema, nifanye nini, niurithi uzima wa kale na kale? Yesu akamwambia: Unaniitaje mwema? Hakuna aliye mwema, asipokuwa Mungu peke yake tu. Maagizo unayajua, ya kwamba: Usiue! Usizini! Usiibe! Usisingizie! Usipunje! Mheshimu baba yako na mama yako! Naye akamwambia: Mfunzi, hayo yote nimeyashika, tangu nilipokuwa kijana. Yesu akamtazama, akampenda, akamwambia: Umesaza kimoja: nenda, uviuze vyote, ulivyo navyo, uvigawie maskini! Hivyo utakuwa na kilimbiko mbinguni. Kisha uje, ujitwishe msalaba wako, unifuate! Lakini alipolisikia neno hili alikunjamana uso, akaenda zake na kusikitika, kwani alikuwa mwenye mali nyingi. Kisha Yesu akatazama huko na huko, akawaambia wanafunzi wake: Vitazameni vigumu vinavyowazuia waegemeao mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Wanafunzi walipoingiwa na kituko kwa hayo mnaneno yake, Yesu akajibu, akawaambia tena: Wanangu, vitazameni vigumu vinavyozuia kuingia katika ufalme wa Mungu! Masumbuko ya ngamia ya kupenya tunduni mwa sindano ni madogo kuliko yake mwenye mali ya kuuuingia ufalme wa Mungu. Nao wakastuka mno, wakasemezana wao kwa wao: Ikiwa hivyo, yuko nani awezaye kuokoka? Yesu akawachungua, akasema: Kwa watu haliwezekani, lakini kwa Mungu linawezekana, kwani kwa Mungu mambo yote huwezekana.* Petero akaanza kumwambia: Tazama, sisi tumeviacha vyote, tukakufuata wewe. Ndipo, Yesu aliposema: Kweli nawaambiani: Hakuna mtu aliyeacha nyumba au kaka au dada au mama au baba au wana au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Utume mwema, asiporudishiwa na kuongezwa mara mia siku hizi za kuwapo huku nchini nyumba na kaka na dada na mama na wana na mashamba, hata akiwa anafukuzwafukuzwa. Tena siku zile zitakazokuja ataupata nao uzima wa kale na kale. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, nao walio wa mwisho watakuwa wa kwanza. Walipokuwa njiani wakipanda kwenda Yerusalemu, Yesu alikuwa anatangulia mbele yao. Nao wakashikwa na kituko, wakamfuata na kuogopa. Akawachukua tena wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia mambo yatakayompata, akasema: Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu. Huko Mwana wa mtu atatiwa mikononi mwao watambikaji wakuu na waandishi, nao watamhukumu, auawe; kwa hiyo watamtia mikononi mwa wamizimu. Ndio watakaomfyoza na kumtemea mate na kumpiga viboko na kumwua. Naye, siku tatu zitakapopita, atafufuka. *Yakobo na Yohana, wana wa Zebedeo, wakamsogelea wakimwambia: Mfunzi, twataka, ufufanyie lo lote, tutakalokuomba. Alipowauliza: Mwataka, niwafanyie nini? wakamwambia: Utuketishe mmoja kuumeni na mmoja kushotoni kwako katika utukufu wako! Yesu akawaambia: Hamjui, mnaloliomba. Mwaweza kukinywa kinyweo, ninachokinywa mimi, au kubatizwa ubatizo, ninaobatizwa mimi? Walipomwambia: Twaweza, Yesu akawaambia: Kinyweo, ninachokinywa mimi, mtakinywa nao ubatizo, ninaobatizwa mimi, mtabatizwa; lakini kumketisha mtu kuumeni au kushotoni kwangu hii si kazi yangu, ila hupewa walioandaliwa. Wenzao kumi walipoyasikia wakaanza kumkasirikia Yakobo na Yohana. Yesu akawaita, wamjongelee, akawaambia: Mnajua: wanaotazamwa kuwa wafalme wa mataifa huwatawala, nao wakubwa wao huwatumikisha kwa nguvu. Kwenu ninyi visiwe hivyo! Ila mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu sharti awe mtumishi wenu! Naye anayetaka kuwa wa kwanza kwenu sharti awe mtumwa wao wote! Kwani naye Mwana wa mtu hakuja, atumikiwe, ila amekuja kutumika na kuitoa roho yake kuwa makombozi ya watu wengi. Wakafika Yeriko. Nao walipotoka Yeriko, yeye na wanafunzi wake na kundi la watu wengi, Bartimeo, mwana wa Timeo, aliyekuwa kipofu alikaa njiani kando akiomba sadaka. Aliposikia, ya kuwa Yesu wa Nasareti yuko, akaanza kupaza sauti na kusema: Yesu, mwana wa Dawidi, nihurumie! Wengi walipomkaripia, anyamaze, yeye akakaza sana kupaza sauti: Mwana wa Dawidi, nihurumie! Ndipo, Yesu aliposimama, akasema: Mwiteni! Wakamwita kipofu, wakamwambia: Tulia moyo, inuka! anakuita. Naye akaitupa kanzu yake, akainuka upesi, akaja kwa Yesu. Yesu alipomwuliza akisema: Wataka, nikufanyie nini? kipofu akamwambia: Mfunzi mkuu, nataka, nipate kuona. Yesu akamwambia: Enenda! Kunitegemea kwako kumekuponya. Mara akapata kuona, akamfuata njiani. Hapo, walipoukaribia Yerusalemu na kufika Beti-Fage na Betania penye mlima wa michekele, akatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia: Nendeni katika kijiji kinachowaelekea! Mtakapoingia mle mara mtaona, pamefungwa mwana punda, ambaye mtu hajampanda bado; mfungueni, mmlete! Kama mtu atawauliza: Mbona mnafanya hivi? semeni: Bwana wetu anamtakia kazi! Mara atawapani, mmlete hapa. Walipoondoka kwenda, wakamwona mwana punda aliyefungwa mlangoni nje njiani, wakamfungua. Wengine waliosimama huko wakawauliza: Mnafanya nini mkimfungua mwana punda? Nao wakajibu, kama Yesu alivyowaambia; ndipo, walipowaacha. Wakampeleka mwana punda kwa Yesu, wakatandika nguo zao upesiupesi juu yake, kisha akampanda. Watu wengi wakatandika nguo zao njiani, wengine wakatandika matawi ya miti, waliyoyakata mashambani. Nao waliotangulia nao waliofuata wakapaza sauti: Hosiana! Na atukuzwe ajaye kwa jina la Bwana! Utukuzwe ufalme wa baba yetu Dawidi utujiao! Hosiana juu mbinguni! Alipoingia Yerusalemu, akaenda Patakatifu. Alipokwisha kuvitazama vyote vilivyomo, mchana ukawa umekuchwa; kwa hiyo akatoka kwenda Betania pamoja na wale kumi na wawili. Kesho yake walipotoka Betania akaona njaa. Huko mbali akaona mkuyu wenye majani, akaenda, aone, kama liko tunda juu yake. Akaufikia, asione kitu, ila majani tu, kwani siku za kuyu hazijawa. Ndipo, alipotoa neno la kwamba: Kale na kale mtu asile tena kwako tunda! Wanafunzi wake wakayasikia. Walipofika Yerusalemu, akapaingia Patakatifu, akaanza kuwafukuza wenye kuuzia na kununulia hapo Patakatifu, akaziangusha meza za wavunja fedha na viti vya wachuuzi wa njiwa. Tena hakuacha, mwenye kuchukua chombo apapitie hapo Patakatifu. Akawafundisha akiwaambia: Haikuandikwa ya kuwa: Nyumba yangu itaitwa nyumba ya kuombea kwao makabila yote ya watu? Lakini ninyi mmeigeuza kuwa pango la wanyang'anyi. Watambikaji wakuu na waandishi walipoyasikia, wakatafuta, watakavyomwangamiza, kwani walimwogopa, kwa sababu watu wote pia walishangazwa na mafundisho yake. Lakini kila siku ilipokuwa jioni, wakatoka mjini. Asubuhi walipopita wakauona mkuyu, umekuwa umekauka toka mizizini. Petero akalikumbuka neno lile, akamwambia: Bwana, tazama, mkuyu, uliouapiza, umenyauka. Yesu akawajibu akisema: Mwe wenye kumtegemea Mungu! Kweli nawaambiani: Kila atakayeuambia mlima huu: Ondoka hapa, ulipo, ujitupe baharini! basi, litatimia vivyo hivyo, asipokuwa na mashaka moyoni mwake, ila akiwa anayategemea tu ya kuwa: Analolisema, litatendeka. Kwa hiyo nawaambiani: Yo yote mnayoyaomba kwa kuyataka, yategemeeni tu, ya kuwa mtayapata! ndipo, mtakapoyapata kweli. Nanyi mtakaposimama na kuomba mwondoleane, mkiwa mnamwekea mtu mfundo, Baba yenu alioko mbinguni naye awaondolee ninyi makosa yenu! Lakini ninyi msipoondoleana, naye Baba alioko mbinguni hatawaondolea makosa yenu. Walipoingia tena Yerusalemu, naye alipotembea Patakatifu, wakamjia watambikaji wakuu na waandishi na wazee, wakamwuliza: Hayo unayafanya kwa nguvu gani? au ni nani aliyekupa nguvu hii, uyafanye hayo? Yesu akawaambia: Nanyi nitawauliza neno moja; mtakaponijibu, nitawaelezea nguvu yangu ya kuyafanya hayo. Ubatizo wake Yohana ulitoka mbinguni au kwa watu? Nijibuni! Wakafikiri mioyoni mwao kwamba: Tukisema: Ulitoka mbinguni, atatuuliza: Mbona hamkumtegemea? Lakini tukisema: Ulitoka kwa watu, basi, waliwaogopa watu; kwani watu wote walimshika Yohana kuwa mfumbuaji wa kweli. Kwa hiyo wakamjibu Yesu wakisema: hatujui. Ndipo, Yesu alipowaambia: Basi, hata mimi siwaambii nguvu inayonifanyisha hayo. Akaanza kusema nao kwa mifano. Mtu alipanda mizabibu, akaizungusha ugo, akachimbua kamulio la kuzikamulia zabibu, ajenga dungu, akaipangisha wakulima, kisha akaenda katika nchi nyingine. Siku zilipotimia, akatuma mtumwa kwa wale wakulima, apewe na wakulima matunda ya mizabibu. Nao wakamkamata, wakampiga, wakamrudisha mikono mitupu. Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, naye wakampiga na kumtia vidonda vya kichwani na kumtukana. Alipotuma tena mwingine, huyo naye wakamwua. Nao wengine wengi, wengine wakawapiga, wengine wakawaua. Alikuwa na mmoja tena, ndiye mwanawe mpendwa; huyo akamtuma kwao wa mwisho akisema: Watamcha mwanangu. Lakini wale wakulima wakasemezana wao kwa wao: Huyu ndiye kibwana, njoni, tumwue! Kisha nao urithi wake utakuwa wetu! Kwa hiyo wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya mizabibu. Basi, mwenye mizabibu atafanya nini? Atakapokuja atawaangamiza wale wakulima, nayo mizabibu atawapa wengine. Hamjalisoma bado andiko hilo la kwamba: Jiwe, walilolikataa waashi, hilihili limekuwa la pembeni? Hivyo vimefanywa na Bwana; nasi tukivitazama, ni vya kustaajabu. Ndipo, walipotafuta kumkamata, lakini waliliogopa kundi la watu. Kwani walitambua, ya kuwa amewasemea wao wenyewe mfano huo. Lakini wakamwacha, wakaenda zao. Wakatuma kwake Mafariseo na watu wa Herode, wamtege kwa maneno yake. Wakaja, wakamwambia: Mfunzi, tumekujua, ya kuwa wewe ni mtu wa kweli, tena humwuliziulizi mtu ye yote, kwani hutazami nyuso za watu, nayo njia ya Mungu unaifundisha, ilivyo kweli. Iko ruhusa ya kumtolea Kaisari kodi au haiko? Tumpe au tusimpe? Kwa kuujua ujanja wao akawaambia: Mwanijaribiaje? Nileteeni shilingi, niitazame! Walipomletea, akawauliza: Chama hiki cha nani? Maandiko nayo ya nani? Wakamwambia: Ni yake Kaisari. Ndipo, Yesu alipowaambia: Yaliyo yake Kaisari mtoleeni Kaisari, naye Mungu yaliyo yake Mungu! Wakamstaajabu sana. Masadukeo wanaosema: Hakuna ufufuko walipokuja kwake wakamwuliza wakisema: Mfunzi, Mose alituandikia kama hivi: Mtu akifiwa na mkubwa wake aliyeacha mkewe, lakini hakuacha mwana, nduguye amchukue huyo mke, amzalie mkubwa wake mwana. Kulikuwa na waume saba walio ndugu. Wa kwanza akaoa mke, lakini alipokufa hakuacha mwana. Wa pili naye akamchukua, akafa, asiache mwana. Naye wa tatu vivi hivi. Nao wote saba hawakuacha mwana. Mwisho wao wote akafa naye mwanamke. Basi, katika ufufuko watakapofufuka, atakuwa mke wa yupi wa hao? Kwani wote saba walikuwa naye yule mwanamke. Yesu akawaambia: Mkipotelewa hivyo, maana hamyajui Maandiko wala nguvu ya Mungu? Kwani watakapofufuka katika wafu hawataoa, wala hawataolewa, ila watakuwa, kama malaika walivyo mbinguni. Lakini kwa ajili ya wafu, kwamba wafufuliwa, hamkusoma katika kitabu cha Mose, Mungu alivyomwambia hapo kichakani: Mimi ni Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo? Basi, Mungu siye wa wafu, ila wao walio hai. Ninyi mnapotelewa sana. Akamjia mwandishi mmoja aliyewasikia, walivyobishana; naye alijua, ya kuwa amewajibu vizuri. Huyo akamwuliza: Katika maagizo yote lililo la kwanza ni lipi? Yesu akajibu: La kwanza ndilo hili: Sikia, Isiraeli! Bwana Mungu wetu ni Bwana peke yake. Nawe umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa mawazo yako yote na kwa nguvu yako yote! La pili ndilo hili: Umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwenyewe! Agizo jingine lililo kubwa kuliko haya haliko. Yule mwandishi akamwambia: Vema, mfunzi, umesema ya kweli: Mungu ni mmoja tu, hakuna mwingine ila yeye. Tena kumpenda yeye kwa moyo wote na kwa mawazo yote na kwa nguvu yote, na kumpenda mwenzio, kama unavyojipenda mwenyewe, hupita ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na vipaji vyote vya tambiko. Yesu alipomwona, ya kuwa amejibu yenye maana, akamwambia: Wewe hu mbali ya ufalme wa Mungu. Kisha hakuwako hata mmoja aliyejipa moyo wa kumwuliza neno tena. Yesu alipofundisha hapo Patakatifu akawauliza akisema: Waandishi husemaje, ya kuwa Kristo ni mwana wa Dawidi? Dawidi mwenyewe alisema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti kuumeni kwangu, mpaka niwaweke adui zako chini miguuni pako! Basi, Dawidi mwenyewe akimwita Bwana, anakuwaje tena mwana wake? Kwa kuwa watu wengi walipendezwa kumsikiliza, akasema na kuwafundisha: Jiangalieni kwa ajili ya waandishi wanaotaka kutembea wenye kanzu ndefu na kuamkiwa na watu sokoni! Namo nyumbani mwa kuombea hupenda viti vya mbele, hata wakialikwa chakulani hupenda kukaa penye wakuu. Huzila nyumba za wajane wakijitendekeza, kama wanakaza kuwaombea. Walio hivyo mapatilizo yao yatakuwa kuliko ya wengine. *Akakaa na kuielekea sanduku ya vipaji, akatazama, watu wanavyotia mapesa katika sanduku ya vipaji. Wenye mali wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mjane mmoja aliyekuwa mkiwa, akatia visenti viwili, pamoja ni hela moja. Ndipo, alipowaita wanafunzi wake, akawaambia: Kweli nawaambiani: Huyu mjane mkiwa ametia mengi kuliko wote waliotia mapesa humu sandukuni mwenye vipaji. Kwani wote walitoa mali katika mali zao nyingi, lakini huyu kwa ukiwa wake amevitoa vyote, alivyokuwa navyo, ndivyo vyote vilivyomlisha.* Alipotoka Patakatifu, mwanafunzi wake mmoja akamwambia: Mfunzi, yatazame mawe hayo makubwa na majengo hayo makubwa! Yesu akamwambia: Je? Wayatazama majengo haya makubwa? Halitaachwa hata jiwe moja juu ya jiwe lenziwe lisiloporomoshwa chini. Kisha alipokaa mlimani pa michekele kupaelekea Patakatifu, ndipo, Petero na Yakobo na Yohana na Anderea walipomwuliza walipokuwa peke yao wakisema: Tuambie, hayo yatakuwapo lini? Tena kielekezo ni nini, hayo yote yatakapotimia? Yesu akaanza kuwaambia: Angalieni, mtu asiwapoteze! Wengi watakuja kwa jina langu na kusema: Mimi ndiye, nao watapoteza wengi. Nanyi mtakaposikia vita na mavumi ya vita msivihangaikie! Hivyo sharti viwepo, lakini huo sio mwisho. Kwani watainukiana taifa na taifa, tena wafalme na wenzao wafalme. Mahali penginepengine patakuwa na matetemeko, pengine na njaa. Hayo ni mwanzo tu wa uchungu. Lakini ninyi jiangalieni wenyewe! Watawapeleka barazani kwao wakuu namo nyumbani mwa kuombea, mpigwe, kisha mtasimamishwa kwa ajili yangu mbele ya mabwana wakubwa na mbele ya wafalme, mje mnishuhudie kwao. Nao Utume mwema sharti utangazwe kwanza kwa mataifa yote. Napo hapo, watakapowatoa na kuwapeleka, msianze kuyahangaikia maneno ya kusema, ila maneno mtakayopewa saa ile yasemeni yaleyale! Kwani si ninyi mnaosema, ila ni Roho Mtakatifu. Itakuwa hivi: ndugu na ndugu watatoana, wauawe, hata baba watawatoa watoto wao, hata watoto watawainukia wazazi wao, wawaue. Nanyi mtakuwa mmechukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka. Hapo ndipo, mtakapochafukwa mioyo mkiona, mwangamizaji atapishaye akisimama mahali pasipompasa; mwenye kupasoma hapa sharti aangalie, ajue maana! Siku zile watakaokuwako Yudea na wakimbilie milimani! Mtu atakayekuwapo nyumbani juu asishuke na kuingia nyumbani mwake kuchukua kilichomo! Naye atakayekuwako shambani asiyarudie yaliyoko nyuma, aichukue nguo yake! Lakini watakaoona vibaya zaidi ndio wenye mimba na wenye kunyonyesha siku zile. Lakini ombeni, hayo yasitimie siku za kipupwe! Kwani siku zile zitakuwa na maumivu makuu kuyapita yote yaliyopatikana tangu mwanzo wa viumbe, Mungu alivyoviumba, mpaka sasa, hata halafu hayatapatikana tena kama hayo. Nazo siku zile kama Bwana hangalizipunguza, hangaliokoka mtu hata mmoja. Lakini kwa ajili ya wale, waliochaguliwa, aliowachagua, amezipunguza siku zile. Hapo mtu akiwaambia: Tazama, huyu hapa ni Kristo! au: Tazama, yule kule! msiitikie! Watainuka makristo wa uwongo na wafumbuaji wa uwongo; nao watafanya vielekezo na vioja, wawapoteze waliochaguliwa, kama inawezekana. Lakini ninyi angalieni! Nimetangulia kuwaambia yote. Lakini siku zile, yale maumivu yatakapopita, jua litakuwa jeusi lenye giza, nao mwezi hautaumulikisha mwanga wake. Nazo nyota zitakuwa zinaanguka toka mbinguni, nazo nguvu za mbingu zitatukutishwa. Hapo ndipo, watakapomwona Mwana wa mtu, anavyokuja katika mawingu mwenye nguvu na utukufu mwingi. Ndipo, atakapowatuma malaika, awakusanye waliochaguliwa naye toka pande zote nne, upepo unapotokea, aanzie mwanzoni kwa nchi, aufikishe mwisho wa mbingu. Jifundisheni mfano kwa mkuyu: matawi yake yanapochipua na kuchanua majani, mnatambua, ya kuwa siku za vuli ziko karibu. Vivyo hivyo nanyi mtakapoyaona hayo, yakiwapo, tambueni, ya kuwa mwisho umewafikia milangoni! Kweli nawaambiani: Kizazi hiki hakitakoma mpaka hapo, yatakapokuwapo hayo yote. Mbingu na nchi zitakoma, lakini maneno yangu hayatakoma. Lakini ile siku au saa yake itakapofikia, mtu hapajui, wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba tu. Angalieni! Kesheni! Kwani hamjui, siku zake zitakapokuwapo. Vinafanana na mtu mwenye kufunga safari aliyeiacha nyumba yake, akawapa watumishi wake nguvu akimgawia kila mtu kazi yake, naye mlinda mlango akamwagiza, akeshe. Basi, hivyo kesheni! Kwani hamjui, mwenye nyumba atakaporudia, kama atakuja jioni au kati ya usiku au jogoo awikapo au mapema. Asije na kuwastusha akiwakuta, mmelala. Hilo, ninalowaambia ninyi, nawaambia wote: Kesheni! Palikuwa pamesalia siku mbili kuwa sikukuu ya Pasaka na ya mikate isiyotiwa chachu. Nao watambikaji wakuu na waandishi wakatafuta kumkamata kwa werevu, wapate kumwua; lakini walisema: Kwanza sikukuu ipite, watu wasije, wakafanya fujo! Naye alipokuwa Betania nyumbani mwa Simoni Mkoma akikaa chakulani, akamjia mwanamke mwenye kichupa chepe cha jiwe kilichojaa mafuta ya maua yanayoitwa Narada; ni yenye bei kubwa, nayo yalikuwa hayakuchanganywa na mengine. Akakivunja kile kichupa, akayamiminia kichwani pake. Mlikuwamo waliochukiwa mioyoni mwao kwamba: Upotevu huu wa haya mafuta mazuri sana ni wa nini? Kwani mafuta haya yangaliwezekana kuuzwa kwa shilingi 300 na kupita, wakapewa maskini! Kwa hiyo wakamfokea sana. Lakini Yesu akasema: Mwacheni! Mbona mnamsikitisha? Amenitendea tendo zuri. Kwani maskini mnao kwenu siku zote, kila mnapotaka mweze kuwafanyia vema; lakini mimi hamwi nami siku zote. Amefanya, alivyoweza; ameanza kuupaka mwili wangu mafuta haya, autengenezee kuzikwa. Kweli nawaambiani: Po pote katika ulimwengu wote, patakapotangazwa huu Utume mwema, patasemwa nacho hiki, alichokitenda yeye, naye akumbukwe. Kisha Yuda Iskariota aliyekuwa mwenzao wale kumi na wawili akaenda zake kwa watambikaji wakuu, amtie mikononi mwao. Nao walipoyasikia wakafurahi, wakaagana naye kumpa fedha. Ndipo, alipotafuta njia iliyofaa, amtoe. Siku ya kwanza ya kula mikate isiyotiwa chachu, watu walipochinjia kondoo ya Pasaka, wanafunzi wake wakamwuliza: Unataka, twende, tukuandalie wapi, uile kondoo ya Pasaka? Akawatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia: Nendeni mjini! Humo mtakutana na mtu anayechukua mtungi wa maji, mfuateni! Mle atakamoingia mwambieni mwenye nyumba: Mfunzi anauliza: Kiko wapi chumba cha kukaa mimi, ndimo niile kondoo ya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu? Ndipo, mwenyewe atakapowaonyesha chumba kikubwa kilichokwisha kutandikwa; namo mle tuandalieni! Wale wanafunzi wakatoka, wakaenda, wakaingia mjini, wakaona, kama alivyowaambia, wakaiandaa kondoo ya Pasaka. Ilipokuwa jioni, akaja pamoja na wale kumi na wawili. Walipokaa wakila, Yesu akasema: Kweli nawaambiani: Mwenzenu mmoja anayekula pamoja nami atanichongea. Wakaanza kusikitika na kumwuliza mmoja mmoja: Ni mimi? Naye akawaambia: Ninyi kumi na wawili mwenzenu aliyetowelea pamoja nami bakulini ndiye. Mwana wa mtu anakwenda njia yake, kama alivyoandikiwa; lakini yule mtu, ambaye Mwana wa mtu atachongewa naye, atapatwa na mambo. Ingalimfalia yule mtu, kama-asingalizaliwa. Walipokuwa wakila, akatwaa mkate, akauombea, akaumega, akawapa, akasema: Twaeni! Huu ndio mwili wangu. Kisha akatwaa kinyweo, akashukuru, akawapa, wakanywa wote humo, akawaambia: Hii ndiyo damu yangu ya Agano Jipya inayomwagwa kwa ajili ya wengi. Kweli nawaambiani: Tangu sasa sitayanywa tena mazao ya mizabibu mpaka siku ile, nitakapoyanywa mapya katika ufalme wa Mungu. Walipokwisha kuimba wakatoka kwenda mlimani pa michekele. Yesu akawaambia: Nyote mtajikwaa, kwani imeandikwa: Nitampiga mchungaji, kondoo watawanyike; lakini nitakapokwisha kufufuliwa nitawatangulia kwenda Galilea. Ndipo, Petero alipomwambia: Ijapokuwa, wote wajikwae, lakini mimi sio. Yesu akamwambia: Kweli nakuambia: Usiku huu wa leo jogoo atakapokuwa hajawika mara mbili, utakuwa umenikana mara tatu. Naye akakaza mno kusema: Hata ijaponipasa kufa pamoja nawe, sitakukana kabisa. Nao wote wakasema vivyo hivyo. Walipofika mahali, jina lake Getisemane, akawaambia wanafunzi wake: Kaeni hapa, mpaka niishe kuomba! Akamchukua Petero na Yakobo na Yohana, akaenda nao, akaanza kuingiwa na kituko na kuhangaika, akawaambia: Roho yangu inaumizwa sana na masikitiko, imesalia kufa tu. Kaeni papa hapa, mkeshe! Akaendelea mbele kidogo, akaanguka chini, akaomba, ikiwezekana, saa hiyo impite, isimfikie. Akasema: Aba baba, yote yanawezekana kwako; kipitishe kinyweo hiki, nisikinywe! Lakini yasifanyike, niyatakayo mimi, ila yafanyike, uyatakayo wewe! Alipokuja akawakuta, wamelala usingizi, akamwambia Petero: Simoni, umelala usingizi? Hukuweza kukesha saa moja tu? Kesheni na kuomba, msije kuingia majaribuni! Roho inataka kuitikia, lakini mwili ni mnyonge. Akaenda tena, akaomba na kusema maneno yaleyale. Alipokuja tena akawakuta, wamelala usingizi, kwani macho yao yalikuwa mazito, hawakujua ya kumjibu. Alipokuja mara ya tatu akawaambia: Mwafuliza kulala usingizi, uchovu uwatoke? Pametimia, saa imefika; tazameni, Mwana wa mtu anatiwa mikononi mwa wakosaji! Inukeni, twende! Tazameni, mwenye kunichongea yuko karibu! Angali akisema, papo hapo akaja Yuda, mmoja wao wale kumi na wawili, pamoja na kundi la watu wengi wenye panga na rungu waliotoka kwa watambikaji wakuu na kwa waandishi na kwa wazee. Lakini mwenye kumchongea alikuwa amewapa kielekezo akisema: Nitakayemnonea ndiye, mkamateni, mwende naye mkimwangalia sana! Naye alipofika, mara akamjia, akasema: Mfunzi mkuu! akamnonea; ndipo, walipomkamata kwa mikono yao. Lakini mmoja wao waliosimama hapo akauchomoa upanga wake, akampiga mtumwa wa mtambikaji mkuu, akamkata sikio. Lakini Yesu akajibu, akawaambia: Mmetoka wenye panga na rungu, mnikamate mimi, kama watu wanavyomwendea mnyang'anyi. Kila siku nilikuwa kwenu hapo Patakatifu nikifundisha, lakini hamkunikamata; lakini yamekuwapo, Maandiko yatimizwe. Hapo waliokuwa naye wakamwacha, wakakimbia wote. Kulikuwa na kijana mmoja aliyefuatana naye, alikuwa ameufunika uchi wake kwa kitambaa cha bafta tu. Lakini walipomkamata, akakiacha kile kitambaa cha bafta, akakimbia mwenye uchi. Wakampeleka Yesu kwa mtambikaji mkuu. Wakakusanyika wote, watambikaji wakuu na wazee na waandishi. Naye Petero akamfuata mbalimbali, mpaka akaingia uani kwa mtambikaji mkuu, akakaa pamoja na watumishi penye mwangaza akiota moto. Lakini watambikaji wakuu na baraza ya wakuu wote wakamtafutia Yesu ushuhuda, wapate kumwua, lakini hawakuupata. Kwani wengi walimshuhudia ya uwongo, lakini ushuhuda wao haukupatana. Kisha wakainuka wengine, wakamshuhudia ya uwongo na kusema: Sisi tumesikia, alivyosema: Mimi nitalivunja Jumba hili la Mungu lililojengwa na mikono, tena nitajenga jingine muda wa siku tatu lisilojengwa na mikono. Lakini hata hivyo ushuhuda wao haukupatana. Ndipo, mtambikaji mkuu alipoinuka, akaja katikati, akamwuliza Yesu akisema: Hujibu neno, hawa wanayokusimangia? Lakini akanyamaza kimya, asimjibu neno. Mtambikaji mkuu akamwuliza tena akimwambia: Wewe ndiwe Kristo, mwana wake Mtukufu? Yesu akasema: Mimi ndiye. Nanyi mtamwona Mwana wa mtu, anavyokaa kuumeni kwa nguvu, tena atakavyokuja na mawingu ya mbinguni. Ndipo, mtambikaji mkuu alipozirarua nguo zake, akasema: Mashahidi tunawatakia nini tena? Mmesikia, anavyombeza Mungu. Mwaonaje? Nao wote wakamhukumu kwamba: Amepaswa na kufa. Kisha wengine wakaanza kumtemea mate, tena wakamfunika uso, wakampiga makonde, wakamwambia: Fumbua! Nao watumishi wakamchukua, wakampiga makofi. Naye Petero alipokuwa amekaa chini uani, akaja mmoja wao vijakazi wa mtambikaji mkuu. Alipomwona Petero, alivyoota moto, akamchungulia, akasema: Hata wewe ulikuwa pamoja na yule Yesu wa Nasareti. Akakana akisema: Sijui, wala sitambui, wewe unayoyasema. Kisha akatoka kufika nje ukumbini. Yule kijakazi alipomwona, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale: Huyu ni mwenzao. Lakini akakana tena. Tena punde kidogo waliosimama pale wakamwambia Petero: Kweli u mwenzao, kwani nawe u Mgalilea. Ndipo, alipoanza kujiapiza na kuapa akisema: Simjui mtu huyo, mnayemsema. Mara hiyo jogoo akawika mara ya pili. Hapo Petero akalikumbuka lile neno, kama Yesu alivyomwambia: Jogoo atakapokuwa hajawika mara mbili, utakuwa umenikana mara tatu. Alipovifikiri akaanza kulia. Asubuhi kulipokucha, papo hapo watambikaji wakuu wakala njama pamoja na wazee na waandishi nao wote wa baraza ya wakuu wote, wakamfunga Yesu, wakampeleka, wakamtia mikononi mwa Pilato. Pilato alipomwuliza: Wewe ndiwe mfalme wa Wayuda? akamjibu akimwambia: Wewe unavyosema, ndivyo. Watambikaji wakuu walipomsuta mengi, Pilato akamwuliza tena: Hujibu neno? Tazama yote, wanayokusuta! Lakini Yesu hakujibu neno tena, ikawa, Pilato akastaajabu. Kwa desturi ya sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, waliyemtaka. Kulikuwako mtu, jina lake Baraba, alifungwa pamoja na watu waliofunga kondo na kuua watu. Watu wengi walipokwenda bomani kwa kutaka, kwanza awafanyie, kama alivyozoea, Pilato akawajibu akisema: Mwataka, niwafungulie mfalme wa Wayuda? Kwani alitambua, ya kuwa watambikaji wakuu walikuwa wamemtoa kwa wivu. Lakini watambikaji wakuu wakalichochea hilo kundi la watu, sharti awafungulie Baraba. Pilato akajibu tena akiwaambia: Basi, nimfanyie nini huyu, mnayemwita mfalme wa Wayuda? Wakapiga kelele tena kwamba: Mwambe msalabani! Pilato alipowauliza: Ni kiovu gani alichokifanya? wakakaza kupiga makelele kwamba: Mwambe msalabani! Ndipo, Pilato, kwa kuwa alitaka kuyafanya yanayopendeza watu, alipowafungulia Baraba, lakini Yesu akamtoa, apigwe viboko, kisha awambwe msalabani. Nao askari wakampeleka, wakamwingiza uani mwa bomani, wakakiita kikosi chote cha askari, wakusanyike. Wakamvika nguo nyekundu, wakasuka kilemba cha miiba, wakamvika kichwani, wakaanza kumwamkia: Pongezi, mfalme wa Wayuda! Kisha wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate, wakampigia magoti na kumwangukia. Walipokwisha kumfyoza, wakamvua ile nguo nyekundu na kumvika nguo zake, wakampeleka nje, waje, wamwambe msalabani. Wakakamata mtu aliyepiga akitoka shambani; ni Simoni wa Kirene, baba yao Alekisandro na Rufu, wakamshurutisha, amchukulie msalaba wake. Wakampeleka mahali pa Golgota, maana yake ni kwamba: Fuvu la kichwa. Wakampa mvinyo iliyochanganyika na manemane, lakini hakunywa. Walipokwisha kumwamba msalabani, wakazigawanya nguo zake na kuzipigia kura, ndizo mtu achukue. Lakini ilikuwa saa tatu, walipomwamba msalabani. Juu yake kulikuwa na andiko la mashtaka yake la kwamba: MFALME WA WAYUDA. Pamoja naye wakawamba misalabani wanyang'anyi wawili, mmoja kuumeni, mmoja kushotoni kwake. Ndipo, lilipotimia lile neno la kwamba: Akahesabiwa kuwa mwenzao wapotovu. Waliopita wakamtukana, wakavitingisha vichwa vyao wakisema: Wewe unayelivunja Jumba la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe, ushuke mtini! Vilevile nao watambikaji wakuu wakamfyoza pamoja na waandishi wakisema wao kwa wao: Wengine aliwaokoa, lakini mwenyewe hawezi kujiokoa. Huyu Kristo, mfalme wa Waisiraeli, ashuke sasa hivi msalabani, tuvione, tupate kumtegemea! Hata wale waliowambwa misalabani pamoja naye wakamtukana. Ilipokuwa saa sita, pakawa na giza katika nchi yote nzima mpaka saa tisa. Ilipokuwa saa tisa, Yesu akapaza sauti sana: Eli, Eli, lama sabaktani? Maana yake ni kwamba: Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Wengine wao waliosimama hapo walipoyasikia wakasema: Tazama, anamwita Elia! Mmoja akapiga mbio, akachovya mwani sikini, akautia katika utete, akamnywesha akisema: Acheni, tuone, kama Elia anakuja kumshusha! Kisha Yesu akatoa sauti kubwa, nayo pumzi ikamtoka. Ndipo, pazia la Jumbani mwa Mungu lilipopasuka toka juu mpaka chini, likawa vipande viwili. Lakini bwana askari aliyesimama hapo na kumwelekea alipoona, pumzi ilivyomtoka, akasema: Kweli, mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwako nao wanawake, walisimama mbali wakitazama. Kati yao walikuwapo Maria Magadalene na Maria, mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome; ndio waliomfuata na kumtumikia yeye, alipokuwa huko Galilea. Palikuwako nao wengine wengi walipanda pamoja naye kwenda Yerusalemu. Ilipokwisha kuwa jioni, kwa sababu ilikuwa andalio, ndio siku ya kutangulia sikukuu, akaja Yosefu wa Arimatia aliyekuwa mkuu mwenye macheo; naye mwenyewe alikuwa akiungoja ufalme wa Mungu. Akajipa moyo, akaingia kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. Pilato akastaajabu aliposikia, ya kuwa amekwisha kufa, akamwita bwana askari, akamwuliza, kama amekwisha kufa. Alipotambulishwa na bwana askari akampa Yosefu mwili wake. Naye akanunua sanda, akamshusha msalabani, akamtia katika ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani, akafingirisha jiwe mlangoni pa kaburi. Nao akina Maria Magadalene na Maria, mama yake Yose, wakatazama, alipowekwa. *Siku ya mapumziko ilipokwisha pita, ndipo, Maria Magadalene na Maria, mama yake Yakobo, na Salome waliponunua manukato, wapate kwenda kumpaka. Siku ya kwanza ya juma asubuhi na mapema wakajidamka, wakaenda kaburini, jua lilipochomoza. Wakasema wao kwa wao: Nani atatufingirishia lile jiwe, litoke mlangoni pa kaburi? Walipotazama wakaona, jiwe limekwisha fingirishwa; kwani lilikuwa kubwa mno. Walipoingia kaburini wakaona kijana, amekaa kuumeni, amejitanda nguo nyeupe, wakaingiwa na kituko. Naye akawaambia: Msistuke! Mnamtafuta Yesu wa Nasareti aliyewambwa msalabani, amefufuliwa, hayumo humu. Patazameni mahali, walipomweka! Lakini nendeni, mwaambie wanafunzi wake na Petero, ya kuwa anawatangulia ninyi kwenda Galilea! Huko ndiko, mtakakomwona, kama alivyowaambia. Wakatoka kaburini, wakakimbia, kwani walikuwa wameshikwa na utetemeko na ushangao. Kisha hawakumwambia mtu neno, kwani waliogopa.* Alipokwisha fufuka asubuhi na mapema siku ya kwanza ya juma, akamtokea kwanza Maria Magadalene, aliyemfukuzia pepo saba. Ndipo, alipokwenda, akawasimulia wale waliokuwa pamoja naye, walipoomboleza na kulia. Nao waliposikia, ya kuwa anaishi, ya kuwa yeye amemwona, hawakuitikia. Kisha akawatokea wenzao wawili kwa sura nyingine, wakitembea kwenda shambani. Nao wakaenda, wakavisimulia wenzi wao wengine, lakini nao hawakuwaitikia. *Mwisho akawatokea wale kumi na mmoja, walipokaa wakila. Akawakaripia, kwa sababu walikuwa wameshindwa na kumtegemea, na kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao, kwani hawakuwaitikia wale waliomwona, ya kuwa amefufuka. Akawaagiza: Nendeni katika nchi zote za ulimwenguni, mwatangazie wote walioumbwa Utume mwema! Anayemtegemea Mungu akibatizwa ataokoka, lakini asiyemtegemea atahukumiwa. Nao wamtegemeao vielekezo vitakavyowafuata ni hivi: kwa Jina langu watafukuza pepo, watasema kwa ndimi mpya, watashika nyoka, hata wakinywa machawi, hayatawaua kabisa; watakapobandikia wagonjwa mikono, ndipo, watakapoponapona. Bwana Yesu alipokwisha kusema nao akachukuliwa na kupazwa mbinguni, akaketi kuumeni kwa Mungu. Kisha wale wakatoka, wakapiga mbiu mahali po pote. Naye Bwana alifanya kazi pamoja nao akilitia Neno lake nguvu na kutenda vielekezo vilivyowafuata.* Wengi walijaribu kuandika masimulio ya mambo yale yaliyotimilika kwetu. Waliyafuatafuata yale waliyoambiwa na wenye kuyaona yote kwa macho yao, yalivyokuwa tangu mwanzo, kwani walikuwa wamelitumikia lile Neno. Sasa nami nimeyafuata na kuyachungua yote mpaka hapo, yalipoanzia, nikaona, inafaa, nikuandikie sawasawa, kama yalivyofuatana, mwenzangu Teofilo, upate kutambua, ya kuwa mambo yale uliyofundishwa ni ya kweli. Siku zile, Herode alipokuwa mfalme wa Wayuda, palikuwa na mtambikaji wa chama cha Abia, jina lake Zakaria, naye mkewe alikuwa na wana wa Haroni, jina lake Elisabeti. Wote wawili walikuwa waongofu machoni pa Mungu, wakaendelea na kuyashika maagizo na maongozi yote ya Bwana, watu wasione la kuwaonya. Lakini walikuwa hawana mtoto, kwani Elisabeti alikuwa mgumba, nayo miaka yao wote wawili ilikuwa mingi. Chama chake kilipofikiwa na zamu, akaenda kufanya kazi yake ya utambikaji mbele ya Mungu; kwa desturi yao ya utambikaji yeye akapata kuvukiza, akaingia katika Jumba la Bwana. Nalo kundi lote la watu wengi lilikuwa nje, wakiombea saa ileile ya kuvukiza. Malaika wa Bwana akamtokea akisimama mezani pa kuvukizia kuumeni kwake. Zakaria alipomwona akahangaika, woga ukamguia; lakini malaika akamwambia: Usiogope, Zakaria! Kwani ombo lako limesikiwa: mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, nawe utamwita jina lake Yohana. Wewe utafurahi na kushangilia, hata wengine wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwani atakuwa mkubwa machoni pa Bwana; pombe na vileo vyo vyote hatakunywa, lakini atajazwa Roho takatifu papo hapo, atakapozaliwa na mama yake. Atageuza wana wa Isiraeli wengi, warudi kwa Bwana Mungu wao. Mwenyewe atamtangulia Bwana akiwa mwenye roho na nguvu za Elia, aigeuze mioyo ya baba, warudi kwa watoto, awageuze nao wabishi, waufuate ujuzi wa waongofu, amlinganyizie Bwana watu waliojitengeneza. Zakaria akamwambia malaika: Haya nitayatambuaje? Maana mimi ni mzee, nayo miaka ya mke wangu imekuwa mingi. Malaika akajibu, akamwambia: Mimi ni Gaburieli ninayesimama mbele ya Mungu; nimetumwa kusema na wewe, nikupigie mbiu hii njema. Tazama, utakuwa bubu, usiweze kusema mpaka siku hiyo, hayo yatakapokuwapo, kwa sababu hukuyaitikia maneno yangu; nayo yatatimia, siku zao zitakapofika. Wale watu waliokuwa wakimngoja Zakaria, wakastaajabu kukawia kwake katika Jumba la Mungu. Alipotoka hakuweza kusema nao; ndipo, walipotambua, ya kuwa yako mambo, aliyoyaona katika Jumba la Mungu. Naye akawapungia kwa mkono, akakaa kuwa bubu. Ikawa, siku za utambikaji wake zilipomalizika, akaondoka, akaenda nyumbani mwake. Lakini baada ya siku zile mkewe Elisabeti akapata mimba, akajificha miezi mitano, akasema: Ndivyo, alivyonitendea Bwana siku hizi akinitazama, aiondoe soni, niliyokuwa nayo kwa watu. Mwezi wa sita malaika Gaburieli akatumwa na Mungu kwenda katika mji wa Galilea, jina lake Nasareti, amfikie mwanamwali aliyeposwa na mume, jina lake Yosefu, wa mlango wa Dawidi; yule mwanamwali jina lake Maria. Alipoingia mwake akasema: Salamu kwako, kwani yako uliyogawiwa! Bwana yuko pamoja na wewe uliye mwenye kipaji kinachovipita vya wanawake wengine. Alipohangaika kwa neno hili akifikiri kwamba: Huyu ananiamkia kwa namna gani? malaika akamwambia: Usiogope, Maria! Kwani umepata gawio jema kwa Mungu. Tazama, utapata mimba, utazaa mtoto mwana mume, nalo jina lake utamwita YESU. Ndiye atakayekuwa mkuu, ataitwa Mwana wake Alioko huko juu, naye Bwana Mungu atampa kiti cha kifalme cha baba yake Dawidi, atautawala mlango wa Yakobo kale na kale, ufalme wake usiwe na mwisho. Maria akamwambia malaika: Hili litakuwaje? kwani sijajua mume. Malaika akajibu akimwambia: Roho Mtakatifu atakujia, nguvu zake Alioko huko juu zitakufunika kama wingu; kwa hiyo hata mtakatifu atakayezaliwa ataitwa Mwana wake Mungu. Tazama, naye ndugu yako Elisabeti ana mimba ya mtoto mume katika uzee wake, mwezi huu ni wake wa sita, tena alikuwa ameitwa mgumba; kwani hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu. Maria akasema: Tazama, mimi ni kijakazi wa Bwana! Yaniwie, kama ulivyosema! Kisha malaika akaondoka kwake. Siku hizo Maria akainuka, akaenda upesi milimani kufika katika mji wa Yuda. Akaingia nyumbani mwa Zakaria, akamwamkia Elisabeti. Ikawa, Elisabeti aliposikia, Maria anavyomwamkia, kitoto kikarukaruka tumboni mwake, kisha Elisabeti akajazwa Roho takatifu, akapaza sauti kwa nguvu akisema: Wewe umebarikiwa kuliko wanawake wengine, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Tena ni kwa sababu gani, mama yake Bwana wangu akinijia? Kwani sauti yako ya kuniamkia iliponiingia masikioni, mara kitoto tumboni mwangu kilirukaruka kwa kushangilia. Wewe uliyemtegemea Mungu utakuwa mwenye shangwe, kwani yatatimizwa hayo, uliyoambiwa na Bwana. Maria akasema: Bwana ndiye, moyo wangu unayemkuza, roho yangu humshangilia Mungu, mwokozi wangu. Maana ameutazama unyenyekevu wa kijakazi wake; kwani tokea sasa itakuwa, wao wa vizazi vyote wanishangilie. Amenifanyia makuu kwa kuwa mnguvu, Jina lake ni takatifu. Huruma yake huwajia vizazi kwa vizazi wamwogopao. Hufanya ya nguvu kwa mkono wake akiwatawanya waliojikweza katika mawazo ya mioyo yao. Huangusha wenye nguvu katika viti vya kifalme, lakini wao walio wanyenyekevu huwapandisha. Walio wenye njaa huwashibisha mema, lakini wenye mali huwaacha, wajiendee mikono mitupu. Alipokumbuka huruma, akamsaidia mtoto wake Isiraeli, kama alivyowaambia baba zetu, akina Aburahamu nao walio uzao wake kwamba: Wawe wa kale na kale! Maria akakaa kwake, yapata miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani kwake. Elisabeti siku zake za kuzaa zilipotimia, akazaa mtoto mume. Majirani zake na ndugu zake waliposikia, ya kuwa Bwana amemwonea huruma nyingi, wakafurahi pamoja naye. Ilipokuwa siku ya nane, wakaja kumtahiri mtoto, wakamwita jina la baba yake: Zakaria. Lakini mama yake akakataa akisema: Sivyo, sharti aitwe Yohana! Wakamwambia: Hakuna mtu katika ndugu zako aitwaye jina hili. Walipompungia baba yake na kumwuliza jina, alilolitaka, mtoto aitwe, akataka kibao, akaandika na kusema: Yohana ndilo jina lake. Wakastaajabu wote. Mara hiyo akafunguka kinywa chake na ulimi wake, akasema na kumtukuza Mungu. Ndipo, woga ulipowashika wote waliokaa kando kando yao; mambo hayo yote yakasimuliwa milimani po pote pa Yudea. Wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakasema: Basi, huyu mtoto atakuwa wa namna gani? Kwani mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye. Baba yake Zakaria akajazwa Roho takatifu, akafumbua yatakayokuwa akisema: *Atukuzwe Bwana Mungu wa Isiraeli! kwani amewakagua wao wa ukoo wake na kuwapatia ukombozi. Ametusimikia pembe ya wokovu katika mlango wa mtoto wake Dawidi, kama alivyosema kale kwa vinywa vya wafumbuaji wake watakatifu. Akatupatia wokovu kwao walio adui zetu namo mikononi mwao wote wanaotuchukia. Aliwahurumia baba zetu, akalikumbuka Agano lake takatifu nacho kiapo chake, alichomwapia baba yetu Aburahamu kwamba: Tupate kukombolewa mikononi mwa adui zetu, tukae pasipo woga na kumtumikia siku zetu zote tukiwa mbele yake wenye utakaso na wongofu. Nawe kitoto, utaitwa mfumbuaji wake Alioko huko juu, utatangulia mbele ya Bwana, uzitengeneze njia zake na kuwatambulisha wao wa ukoo wake wokovu wao, ya kuwa uko katika kuondolewa makosa yao. Tukivipata hivi, ni kwa huruma zilizomo moyoni mwake Mungu wetu; kwa hiyo umetukagua mwanga unaotoka juu, uwaangaze wanaokaa gizani kwenye kivuli kuuacho, uelekeze miguu yetu, ishike njia ya utengemano. Yule mtoto alipokua akapata nguvu Rohoni, akakaa nyikani mpaka siku, alipowatokea Waisiraeli.* *Ikawa siku zile, amri ikitoka kwa Kaisari Augusto, walimwengu wote waandikiwe kodi; huko kuandikwa kulikuwa kwa kwanza, kukawa siku zile, Kirenio alipotawala Ushami. Ndipo, watu wote waliposhika njia za kwenda kuandikiwa kodi, kila mtu akaenda mjini kwao. Yosefu naye akaondoka Galilea katika mji wa Nasareti kwenda Yudea katika mji wa Dawidi unaoitwa Beti-Lehemu, kwa kuwa yeye alikuwa wa mlango na wa udugu wa Dawidi. Akaenda pamoja na mkewe Maria aliyeposwa naye, waandikiwe kodi; naye alikuwa ana mimba. Ikawa, walipokaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia. Akamzaa mwana wake wa kwanza, ni wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza waliamo ng'ombe, kwani hawakupata pengine nyumbani mwa wageni. Kulikuwa na wachungaji katika nchi ileile, walilala malishoni na kulilinda kundi lao kwa zamu ya usiku. Ndiko, malaika wa Bwana alikowatokea, nao utukufu wa Bwana ukawamulikia po pote, wakashikwa na woga mwingi. Lakini malaika akawaambia: Msiogope! kwani tazameni, ninawapigia mbiu njema yenye furaha kuu itakayowajia watu wote. Kwani mmezaliwa leo mwokozi wenu katika mji wa Dawidi, ndiye Bwana Kristo. Nacho kielekezo chenu ni hiki: mtaona kitoto kichanga, kimevikwa nguo za kitoto, kimelazwa waliamo ng'ombe. Mara wakawa pamoja na yule malaika wingi wa vikosi vya mbinguni, wakamsifu Mungu wakiimba: Utukufu ni wa Mungu mbinguni juu, nchini uko utengemani kwa watu wampendezao. *Ikawa, malaika walipoondoka kwao kwenda mbinguni, wachungaji wakasemezana wao kwa wao: Haya! Twende, tufike hata Beti-Lehemu, tulitazame jambo hilo lililokuwapo, Bwana alilotutambulisha! Wakaenda mbio, wakawakuta, akina Maria na Yosefu na kitoto kichanga, kimelazwa waliamo ng'ombe. Walipokwisha kumwona wakalitambulisha lile neno, waliloambiwa na kitoto hiki. Ndipo, wote walioyasikia walipoyastaajabu, waliyoambiwa na wachungaji. Lakini Maria akayashika maneno hayo yote, akayaweka moyoni mwake na kuyawaza. Kisha wachungaji wakarudi wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa yote, waliyoyasikia, kwani waliona, ni vivyo, kama walivyoambiwa.* *Siku nane za kumtahiri zilipotimia, akaitwa jina lake YESU, lililotajwa na malaika, mama yake alipokuwa hajapata mimba yake.* *Siku zao zilipotimia za weuo, aliouagiza Mose, wakampeleka Yerusalemu, wamtokeze kwake Bwana. Ndivyo, ilivyoandikwa katika Maonyo ya Bwana: Kila mtoto mume atakayezaliwa wa kwanza na mama yake aitwe mtakatifu wa Bwana! Wakatoa vipaji vya kumkomboa, kama ilivyoagizwa katika Maonyo ya Bwana, hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga. *Huko Yerusalemu kulikuwa na mtu, jina lake Simeoni. Mtu huyo alikuwa mwongofu mwenye kumcha Mungu, akaungoja utulivu wa Isiraeli; nayo Roho takatifu ilikuwa naye. Huyo alikuwa amefumbuliwa na Roho Mtakatifu kwamba: Hutaona kufa usipomwona kwanza Kristo wa Bwana. Basi, akaja Patakatifu kwa kuongozwa na Roho. Wazazi walipoingia na mtoto Yesu, wamfanyie, kama walivyozoezwa na Maonyo, mwenyewe akampokea mikononi pake, akamtukuza Mungu akisema: Bwana, sasa unampa mtumwa wako ruhusa, aende zake na kutulia, kama ulivyosema. Kwani macho yangu yameuona wokovu wako, ulioutengeneza machoni pa makabila yote: ni mwanga wa kuwamulikia wamizimu, ukoo wako wa Isiraeli utukuzwe.* Baba yake na mama yake walipokuwa wakiyastaajabu aliyosemewa, Simeoni akawabariki, akamwambia Maria, mama yake: Tazama, huyu ndiye aliyewekewa, wengi walio Waisiraeli waangushwe naye, nao wengine wengi wainuliwe naye; tena amewekewa kuwa kielekezo kinachobishiwa. Nawe wewe upanga utakuchoma moyoni, kusudi mawazo yao wengi yaliyomo mioyoni mwao yafunuke. Kukawa na mfumbuaji wa kike, jina lake Ana, binti Fanueli, wa shina la Aseri. Huyo miaka yake ilikuwa mingi sana; alikuwa amekaa pamoja na mumewe miaka saba baada ya kuwa manamwali. Tena siku hizo alikuwa mjane mwenye miaka 84, lakini hakuondoka Patakatifu akimtumikia Mungu usiku na mchana kwa kufunga na kuombea watu. Naye akawajia saa ileile, akamshukuru Mungu waziwazi, akawaambia mambo ya huyo mtoto wote walioungoja ukombozi wa Yerusalemu. Walipokwisha kuyamaliza yote yaliyoagizwa na Maonyo ya Bwana wakarudi Galilea mjini kwao Nasareti. Lakini yule mtoto akakua, akapata nguvu ya Roho na werevu wote wa kweli, naye Mungu akamgawia mema yake.* *Wazazi wake huenda Yerusalemu kila mwaka kula sikukuu ya Pasaka. Naye alipopata miaka 12, wakakwea naye, kama walivyozoea kwenye hiyo sikukuu. Zile siku zilipomalizika, wakarudi, lakini mtoto wao Yesu akasalia Yerusalemu, wazazi wake wasijue. Wakadhani, yumo katika wenzake wa njiani. Wakaenda mwendo wa siku moja, kisha wakamtafuta kwa ndugu zao na kwa wenzi wao. Wasipomwona wakarudi Yerusalemu wakimtafuta. Siku tatu zilipopita, wakamwona Patakatifu, amekaa katikati ya wafunzi akiwasikiliza na kuulizana nao, nao wote waliomsikia wakaustukia sana ujuzi wake wa kujibu. Walipomwona wakashangaa, mama yake akamwmbia: Mwanangu, mbona umetufanyia hivyo? Tazama, baba yako na mimi tumekutafuta kwa uchungu. Akawaambia: Mwanitafutiani? Hamkujua, ya kuwa imenipasa kuwa mwake Baba yangu? Wao hawakulijua maana neno hili, alilowaambia. Kisha akatelemka pamoja nao, akafika Nasareti, akakaa na kuwatii. Naye mama yake akayashika maneno hayo yote moyoni mwake. Yesu akakua na kuongezeka werevu wa kweli, mpaka akiwa mtu mzima, tena akawa akimpendeza Mungu na watu.* Mwaka wa 15 wa kutawala kwake Kaisari Tiberio Pontio Pilato alikuwa mtawala nchi ya Yudea, naye Herode alikuwa mfalme wa Galilea, naye Filipo, ndugu yake, alikuwa mfalme wa Iturea na wa nchi ya Tarakoniti, naye Lisania alikuwa mfalme wa Abilene, tena Ana na Kayafa walikuwa watambikaji wakuu. Hapo ndipo, neno la Mungu lilipomjia Yohana, mwana wa Zakaria, huko nyikani. Akaenda katika nchi zote za kando ya Yordani, akatangaza ubatizo wa kujutisha, wapate kuondolewa makosa. Ikawa, kama ilivyoandikwa kitabuni mwa maneno ya mfumbuaji Yesaya: Iko sauti ya mtu apigaye mbiu nyikani: Itengenezeni njia ya Bwana! Yanyosheni mapito yake! Vibonde vyote vifukiwe, navyo vilima vyote na vichuguu vyote vichimbuliwe! Napo palipopotoka panyoshwe, napo penye mashimo pawe njia za sawasawa, wote wenye miili wauone wokovu wake Mungu. Akawaambia makundi ya watu waliotokea, wabatizwe naye: Ninyi wana wa nyoka, nani aliwaambia ninyi, ya kuwa mtayakimbia makali yatakayokuja? Tendeni mazao yaliyo ya kujuta kweli! Msianze kusema mioyoni mwenu: Tunaye baba yetu, ndiye Aburahamu! Kwani nawaambiani: Katika mawe haya ndimo, Mungu awezamo kumwinulia Aburahamu wana. Miti imekwisha wekewa mashoka mashinani, kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa, utupwe motoni. Yale makundi ya watu wakamwuliza wakisema: Basi, tufanye nini? Akajibu akiwaambia: Mwenye nguo mbili amgawie mwenziwe asiye nayo, naye mwenye vyakula na afanye vilevile! Watoza kodi nao walipokuja, wabatizwe, wakamwuliza: Mfunzi, tufanye nini? Naye akawaambia: Msitoze kuvipita hivyo, mlivyoagizwa! Walipomwuliza nao askari wakisema: Nasi tufanye nini? akawaambia: Msimwendee mtu kwa nguvu wala kwa ukorofi, tena mtoshewe na mishahara yenu! Watu walipokuwa wakingoja, vya Yohana vitakapotokea wazi, wote waliwaza mioyoni mwao kwamba: Yeye labda ni Kristo; ndipo, Yohana aliposema akiwaambia wote: Mimi nawabatiza kwa maji; lakini anakuja aliye na nguvu kunipita mimi, nami sifai kumfungulia kanda za viatu vyake. Yeye atawabatiza katika Roho takatifu na katika moto. Ungo wa kupepetea umo mkononi mwake, apafagie pake pa kupuria ngano; ngano atazikusanya, aziweke chanjani mwake, lakini makapi atayachoma kwa moto usiozimika. Hivyo aliwapigia watu mbiu njema na kuwaonya hata mengine mengi. Lakini mfalme Herode alipoumbuliwa naye kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, na kwa ajili ya mabaya yote, Herode aliyoyatenda, akayaongeza mabaya yake na kumfunga Yohanba kifungoni. Lakini watu wote walipokuwa wakibatizwa, Yesu anaye alipobatizwa, ikawa, alipokuwa katika kuomba, ndipo, mbingu zilipofunuka, Roho Mtakatifu akamshukia mwenye mwili kama wa njiwa, sauti ikatoka mbinguni: Wewe ndiwe mwanangu mpendwa, nimependewa na wewe. Yesu alipoianza kazi yake alikuwa wa miaka kama 30. Akadhaniwa kuwa mwana wa Yosefu, wa Eli, wa Matati, wa Lawi, wa Melki, wa Yanai, wa Yosefu, wa matatia, wa Amosi, wa Nahumu, wa Esili, wa Nagai, wa Mahati, wa Matatia, wa Simei, wa Yoseki, wa Yoda, wa Yohana, wa Resa, wa Zerubabeli, wa Saltieli, wa Neri, wa Melki, wa Adi, wa Kosamu, wa Elmadamu, wa Heri, wa Yesu, wa Eliezeri, wa Yorimu, wa Matati, wa Lawi, wa Simeoni, wa Yuda, wa Yosefu, wa Yonamu, wa Eliakimu, wa Melea, wa Mena, wa Matata, wa Natani, wa Dawidi, wa Isai, wa Obedi, wa Boazi, wa Salmoni, wa Nasoni, wa Aminadabu, wa Ramu, wa Hesiromu, wa Peresi, wa Yuda, wa Yakobo, wa Isaka, wa Aburahamu, wa Tera, wa Nahori, wa Serugi, wa Ragau, wa Pelegi, wa Eberi, wa Sala, wa Kenani, wa Arpakisadi, wa Semu, wa Noa, wa Lameki, wa Metusela, wa Henoki, wa Yaredi, wa Mahalaleli, wa Kenani, wa Enosi, wa Seti, wa Adamu wa Mungu. Yesu akajaa Roho takatifu, akarudi akitoka huko Yordani, akapelekwa na Roho nyikani, akajaribiwa siku 40 na Msengenyaji. Siku zile hakula cho chote; zilipokwisha pita, akaona njaa. Msengenyaji akamwambia: Kama ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili, liwe chakula! Yesu akamjibu akisema: Imeandikwa: Mtu hataishi kwa chakula tu, ila kwa kila neno la Mungu. Kisha akampandisha mlimani, akamwonyesha kwa kitambo kidogo ufalme wote pia wa ulimwengu. Kisha Msengenyaji akamwambia: Nguvu hii yote na utukufu wake nitakupa wewe; kwani mimi nimepewa, nami humpa ye yote, nimtakaye. Basi, wewe ukiniangukia hapa machoni pangu, yote yatakuwa yako. Yesu akajibu akimwambia: Ondoka nyuma yangu, Satani! Imeandikwa: Umwangukie Bwana Mungu wako na kumtumikia peke yake! Kisha akampeleka Yerusalemu, akamsimamisha juu pembeni hapo Patakatifu, akamwambia: Kama ndiwe Mwana wa Mungu, ruka hapa, ujitupe chini! Kwani imeandikwa: Atakuagizia malaika zake, wakulinde, nao watakuchukua mikononi mwao, usije kujikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akajibu akimwambia: Liko neno la kwamba: Usimjaribu Bwana Mungu wako! Msengenyaji alipokwisha kumjaribu yote akaondoka, akamwacha kwanza. Yesu akarudi Galilea mwenye nguvu ya Roho, akavumika katika nchi zote zilizoko pembenipembeni. Naye alipofundisha katika nyumba zao za kuombea akatukuzwa nao wote. *Alipofika Nasareti, - ndio mji, alimolelewa, - akaingia siku ya mapumziko nyumbani mwa kuombea, kama alivyozoea. Alipoinuka kuwasomea akapewa kitabu cha mfumbuaji Yesaya; alipokifunua hicho kitabu akaona mahali palipolandikwa: Roho ya Bwana inanikalia, kwa hiyo ameanipaka mafuta, niwapigie maskini mbiu njema. Amenituma, niwatangazie mateka, ya kuwa watakombolewa, nao vipofu, ya kuwa wataona, niwape ruhusa walioumizwa, wajiendee, niutangaze mwaka wa Bwana upendezao. Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi, akaketi. Ndipo, wote waliokuwamo humo nyumbani mwa kuombea walipomkazia macho, akaanza kuwaambia: Leo hivi yaliyoandikwa hapa yametimia masikioni penu.* Nao wote wakamshuihudia ya kuwa ndivyo, wakastaajabu maneno ya upole yaliyotoka kinywani mwake, wakasema: Huyu si mwana wa Yosefu? Akawaambia: Kweli mtaniambia fumbo hili: Mganga, jiponye mwenyewe! Hata huku kwako, ulikokulia, yafanye, tuliyoyasikia, ya kuwa yamefanyika Kapernaumu! Lakini akasema: Kweli nawaambiani: Hakuna mfumbuaji anayepokelewa kwao, alikokulia. Nawaambiani ya kweli: Siku za Elia kulikuwa na wajane wengi katika Waisiraeli; ni hapo, mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, ikawa njaa kubwa katika nchi zote. Lakini hao Elia hakutumwa kwa mwenzao mmoja, ila alitumwa Sareputa wa Sidoni kwa mwanamke mjane wa kule. Tena siku za mfumbuaji Elisa kulikuwa na wenye ukoma wengi katika Waisiraeli, lakini kwao hao hakuna aliyetakaswa ila Namani wa Ushami. Wote waliokuwamo humo nyumbani mwa kuombea walipoyasikia haya, mioyo yao ikajaa makali, wakainuka, wakamfukuza mjini, wakampeleka ukingoni pa mlima, ambao mji wao ulikuwa umejengwa juu yake, wapate kumsukuma chini. Lakini yeye akapita katikati yao, akaenda zake. Akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilea, akawa akiwafundisha siku ya mapumziko. Nao wakashangazwa na mafundisho yake, kwani maneno yake yalikuwa yenye nguvu. Humo nyumbani mwa kuombea mkawa na mtu mwenye pepo mchafu, akapaza sauti na kupiga kelele: Acha! Tuko na jambo gani sisi na wewe, Yesu wa Nasareti? Umekuja kutuangamiza. Nakujua, kama u nani; ndiwe Mtakatifu wa Mungu. Yesu alipomkaripia akisema: Nyamaza, umtoke! ndipo, yule pepo alipomkumba, aanguke katikati, kisha akamtoka pasipo kumwumiza. Wote wakaingiwa na kituko, wakasemezana wao kwa wao wakiuliza: Neno gani hilo? Anawaagiza pepo wachafu kwa nguvu ya kifalme, nao hutoka! Huo uvumi wake ukatoka, ukafika po pote penye nchi zilizoko pembenipembeni. Alipoondoka nyumbani mwa kuombea akaingia nyumbani mwa Simoni. Naye mama ya mkewe Simoni alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwombea kwake. Akaja, akasimama kichwani pake, akaikaripia homa; ndipo, ilipomwacha. Papo hapo akainuka kitandani, akawatumikia. Jua lilipokuchwa, wakaja wote waliokuwa na wanyonge wa magonjwa menginemengine, wakiwaleta kwake; akawaponya kwa kuwabandikia mikono kila mmoja. Hata pepo wakatoka wengi wakipiga kelele na kusema: Wewe ndiwe Mwana wa Mungu. Lakini akawakaripia, akawakataza kusema, ya kuwa walimjua kuwa yeye ni Kristo. Lakini kulipokucha, akatoka, akaenda mahali palipokuwa pasipo watu. Ndipo, makundi ya watu walipomtafuta, wakaja kwake, wakamzuia, asiondoke kwao. Lakini akawaambia: Inanipasa kuipigia hata miji mingine mbiu njema ya ufalme wa Mungu, kwani hiyo ndiyo, niliyotumiwa. Kisha akawa akiipiga hiyo mbiu katika nyumba za kuombea zilizoko Galilea. *Ikawa, kundi la watu lilipomsonga na kulisikia Neno la Mungu, alikuwa amesimama ufukoni pa ziwa la Genesareti, akaona vyombo viwili, vimekaa ufukoni, nao wavuvi walikuwa wameshuka wakiziosha nyavu zao. Ndipo, alipoingia katika chombo kimoja kilichokuwa cha Simoni, akamwomba, akisogeze mbali kidogo hapo ufukoni. Akakaa katika chombo akiwafundisha makundi ya watu. Alipokwisha kusema nao akamwambia Simoni: Peleka chombo kilindini, mzishushe nyavu zetu mvue samaki! Simoni akajibu akisema: Bwana, usiku kucha tumesumbuka kwa kazi, tusipate kitu; lakini kwa agizo lako wewe nitazishusha nyavu. Walipovifanya hivyo wakakamata samaki wengi sana, nyavu zao zikakatikakatika. Ndipo, walipowapungia wenzi wao waliokuwa katika chombo kingine, waje kuwasaidia, nao wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, vikafikia kuzama. Simoni Petero alipoyaona hayo akampigia Yesu magoti, akasema: Ondoka kwangu, Bwana! kwani mimi ni mtu mkosaji. Kwani kituko kilikuwa kimemshika yeye nao wote waliokuwa pamoja naye, kwa hivyo, walivyokamata samaki wengi; akina Yakobo na Yohana, wana wa Zebedeo, ndio waliokuwa wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni: Usiogope! Toka sasa utakuwa ukivua watu. Walipokwisha kuvipeleka vyombo uvukoni, wakayaacha yote wakamfuata yeye* Ikawa, alipokuwa kule kwenye miji ile, mara kulikuwako mtu aliyeenezwa mwili wote na ukoma. Naye alipomwona Yesu akamwangukia kifudifudi, akamwomba akisema: Bwana, ukitaka waweza kunitakasa. Ndipo, aliponyosha mkono, akamgusa akisema: Nataka, utakaswe. Mara ukoma ukamwondoka. Kisha akamkataza, asimwambie mtu neno, akasema: Uende zako, ujionyeshe kwa mtambikaji, utoe kipaji kwa ajili ya kutakaswa kwako, kama Mose alivyoagiza, kije kinishuhudie kwao! Lakini uvumi wake ukafuliza kuendelea, wakakusanyika makundi ya watu wengi, wamsikilize wakiponywa magonjwa yao. Lakini yeye akajiepua, akaenda mahali palipokuwa pasipo watu, akawapo akiomba. Ikawa siku moja, alipokuwa akifundisha, wakakaa naye Mafariseo na wafunzi wa Maonyo waliokuwa wametoka kila mji wa Galilea na Yudea na Yerusalemu. Nayo nguvu ya Mungu ilikuwa naye ya kuponya wagonjwa. Papo hapo wakaja watu wakileta mtu aliyelala kitandani mwenye ugonjwa wa kupooza. Wakajaribu kumwingiza nyumbani na kumweka mbele yake. Wasipoona pa kumwingizia kwa ajili ya watu wengi wakapanda katika paa la nyumba, wakafumua vigae, wakamshusha hapo pamoja na kitanda chake, wakamweka katikati mbele ya Yesu. Alipoona, walivyomtegemea, akasema: Mwenzangu, umeondolewa makosa yako. Ndipo, waandishi na Mafariseo walipoanza kuwaza wakisema: Nani huyu anayesema maneno ya kumbeza Mungu? Yuko nani awezaye kuondoa makosa? Siye Mungu peke yake tu? Kwa kuyatambua hayo mawazo yao Yesu akajibu akiwaambia: Mnawaza nini mioyoni mwenu? Kilicho chepesi ni kipi? kusema: Umeondolewa makosa yako! au kusema: Inuka, uende? Lakini kusudi mpate kujua, ya kuwa Mwana wa mtu ana nguvu ya kuondoa makosa nchini, akamwambia mwenye kupooza: Nakuambia: Inuka, jitwishe kitanda chako, uende nyumbani kwako! Papo hapo akainuka machoni pao, akajitwisha kitanda, alichokilalia, akaenda nyumbani kwake akimtukuza Mungu. Ndipo, wote walipostuka sana, wakamtukuza Mungu, wakashikwa na woga mwingi wakisema: Utukufu, tuliouona leo, sio wa kuujua. Kisha alipotoka kwenda zake akaona mtoza kodi, amekaa forodhani, jina lake Lawi. Akamwambia: Nifuata! Naye akayaacha yote, akainuka, akamfuata. Kisha Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake, mkawamo na kundi jingi la watoza kodi na wengine, wakakaa chakulani pamoja nao. Mafariseo na waandishi wao wakanung'unika, wakawaambia wanafunzi wake: Kwa nini mnakula, tena mnakunywa pamoja na watoza kodi na wakosaji? Yesu akajibu akiwaambia: Walio wazima hawapaswi na mganga, ila walio wagonjwa. Sikujia kuwaita waongofu, ila wakosaji, wajute. Kisha wakamwambia: Wanafunzi wa Yohana hukaza kufunga na kuomba, vilevile nao wanafunzi wa Mafariseo, lakini wanafunzi wako hula, hunywa. Yesu akawaambia: Hamwezi kuwafungisha walioalikwa arusini, bwana arusi akingali pamoja nao. Lakini siku zitakuja, watakapoondolewa bwana arusi; siku zile ndipo, watakapofunga. Kisha akawaambia mfano, ya kuwa hakuna mtu akataye kiraka cha nguo mpya na kukitia katika kanzu chakavu. Kama anafanya hivyo, anaikata ile mpya, nacho kiraka cha nguo mpya hakipatani na ile chakavu. Wala hakuna mtu anayetia mvinyo mpya katika viriba vichakavu; kwani akiitia mle, mvinyo mpya itavipasua viriba, nayo yenyewe itamwagika, navyo viriba vitaangamia. Ila mvinyo mpya hutiwa katika viriba vipya. Wala hakuna aliyekunywa mvinyo ya kale, akitaka mpya, kwani husema: ile ya kale ndiyo nzuri. Akawa akipita katika mashamba siku ya mapumziko; l nao wanafunzi wake wakakonyoa masuke, wakayafikicha kwa mikono, wakala. Lakini walikuwako Mafariseo waliosema: Mbona mnafanya yaliyo mwiko siku ya mapumziko? Yesu akawajibu akisema: Hamkuvisoma hata hivyo, Dawidi alivyovifanya, walipoona njaa yeye nao wenziwe waliokuwa pamoja naye? Hapo aliingia Nyumbani mwa Mungu, akaitwaa mikate aliyowekewa Bwana, akaila, akawapa nao wenziwe. Nayo kuila ni mwiko, huliwa na watambikaji peke yao. Akawaambia: Mwana wa mtu ni bwana wa siku ya mapumziko. Ikawa siku nyingine ya mapumziko, akaingia nyumbani mwa kuombea, akafundisha. Mle mlikuwa na mtu, ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umekaukiana. Waandishi na Mafariseo wakamtunduia, kama atamponya siku ya mapumziko, waone neno la kumsuta. Naye akayajua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliokaukiana: Inuka, usimame hapa katikati! Akainuka, akasimama hapo. Kisha Yesu akawaambia: Nawauliza ninyi: Iko ruhusa siku ya mapumziko kufanya mema au kufanya maovu? kuponya roho ya mtu au kuiangamiza? Akawatazama wote waliokuwako, akamwambia: Unyoshe mkono wako! Alipovifanya, huo mkono wake ukageuka kuwa mzima. Wale wakawa kama wenye wazimu, wasijue kitu, wakasemezana wao kwa wao, watakayomtendea Yesu. Ikawa siku zile, akatoka kwenda mlimani kuomba; akakesha kucha katika kumwomba Mungu. Kulipokucha, akawaita wanafunzi wake, akachagua miongoni mwao kumi na wawili; ndio aliowapa jina la Mitume. Ni Simoni, aliyempa jina la Petero, na Anderea nduguye, na Yakobo na Yohana na Filipo na Bartolomeo na Mateo na Toma na Yakobo wa Alfeo na Simoni aliyeitwa Zelote na Yuda wa Yakobo na Yuda Iskariota, ndiye aliyekuwa mchongezi. Akashuka pamoja nao, akasimama mahali penye uwanda; hapo palikuwa na kundi zima la wanafunzi wake wengi na watu wengine wengi sana waliotoka Yudea po pote na Yerusalemu na pwani pa Tiro na Sidoni; ndio waliokuja, wamsikilize yeye, waponywe magonjwa yao. Nao waliosumbuliwa na pepo wachafu wakaponywa. Wale watu wote wakatafuta kumgusa tu, kwani nguvu zilizotoka kwake ziliwaponya wote. Kisha akainua macho, akawatazama wanafunzi wake, akasema: Wenye shangwe ni ninyi mlio maskini, maana ufalme wa Mungu ni wenu. Wenye shangwe ni ninyi mnaoona njaa sasa, maana mtashibishwa. Wenye shangwe ni ninyi, watu watakapowachukia na kuwatenga kwao na kuwatukana na kuyakataa majina yenu kwa kuwa mabaya kwa ajili ya Mwana wa mtu. Furahini siku ile na kurukaruka! Kwani tazameni, mshahara wenu ni mwingi mbinguni! Kwani hivyo ndivyo, baba zao walivyowafanyia wafumbuaji. Lakini yatawapata ninyi wenye mali, kwani mmekwisha upata utulivu wenu. Yatawapata nanyi mnaoshiba sasa, kwani mtaona njaa. Yatawapata ninyi mnaocheka sasa, kwani mtasikitika na kulia. Yatawapata ninyi, watu wote wanapowaendea kwa maneno mazuri, kwani hivyo ndivyo, baba zao walivyowafanyia wafumbuaji wa uwongo. Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu! Wafanyieni mazuri wanaowachukia! Wabarikini wanaowaapiza! Waombeeni wanaowabeza! Mtu akikupiga kofi shavu moja, umgeuzie la pili, alipige nalo! Mtu anayekunyang'anya kanzu yako, usimkataze kuichukua hata shuka! Kila anayekuomba umpe, naye akunyang'anyaye mali zako, usizitake tena kwake! Kama mnavyotaka, watu wawafanyie ninyi, nanyi mwafanyie vivyo hivyo! Maana mkiwapenda wanaowapendani mnawagawia nini? Kwani nao wakosaji huwapenda wawapendao. Nanyi mnapowafanyia mema wanaowafanyia mema ninyi mnawagawia nini? Nao wakosaji hufanya hivyo hivyo. Nanyi mnapokopesha watu, mnaowangojea kurudishiwa nao, mnawagawia nini? Nao wakosaji huwakopesha wakosaji wenzao, warudishiwe yaleyale. Lakini wapendeni wachukivu wenu! Wafanyieni mema na kuwakopesha, msiowangojea kurudishiwa cho chote! Hivyo mshahara wenu utakuwa mwingi, nanyi mtakuwa wana wake Alioko huko juu. Kwani yeye huwagawia nao wenye majivuno nao wenye ubaya. *Mgeuke kuwa wenye huruma, kama Baba yenu alivyo mwenye huruma! Msiumbue watu, nanyi msije mkaumbuliwa! Msionee watu, nanyi msije mkaonewa! Wafungueni watu, nanyi mje mkafunguliwa! Wapeni watu, nanyi mje mkapewa! Kipimo kizuri kilichoshindiliwa na kutingishwa na kumwagika mtapewa, mfutikie katika nguo zenu. Kwani kipimo, mnachokipimia wengine, ndicho, mtakachopimiwa nanyi tena. Akawaambia mfano: Je? Kipofu aweza kumwongoza kipofu mwenziwe? Hawatatumbukia wote wawili shimoni? Mwanafunzi hampiti mfunzi wake, lakini kila aliyekwisha fundishwa atakuwa, kama mfunzi wake alivyo. Nawe unakitazamiani kibanzi kilichomo jichoni mwa ndugu yako, lakini gogo lililomo jichoni mwako wewe mwenyewe hulioni? Unawezaje kumwambia ndugu yako: Ngoja, ndugu yangu, nikitoe kibanzi kilichomo jichoni mwako? Nalo gogo lililomo jichoni mwako mwenyewe hulioni? Mjanja, kwanza litoe gogo katika jicho lako! Kisha utazame vema, ndivyo upate kukitoa kibanzi kilichomo jichoni mwa ndugu yako!* Kwani hakuna mti mzuri unaozaa matunda maovu; tena hakuna mti mwovu unaozaa matunda mazuri. Kwani kila mti hutambulikana kwa matunda yake mwenyewe. Kwani hawachumi kuyu miibani, wala hawachumi zabibu katika mikunju. Mtu mwema hutoa mema katika kilimbiko chake chema cha moyo, lakini naye mbaya hutoa mabaya katika mabaya yake. Kwani moyo unayoyajaa ndiyo, kinywa cha mtu kinayoyasema. Tena mnaniitiani: Bwana! Bwana! msipoyafanya, ninayoyasema? Kila anayekuja kwangu na kuyasikia maneno yangu na kuyafanyiza, nitawaonyesha, anavyofanana navyo. Amefanana na mtu aliyejenga nyumba, akiichimbia chini vizuri na kuweka msingi mwambani. Maji yalipojaa yakatoka mto, ukapasua penye ile nyumba, lakini haukuweza kuitingisha, kwa kuwa ilikuwa imejengwa vizuri. Lakini anayeyasikia asipoyafanyiza amefanana na mtu aliyejenga nyumba mchangani pasipo msingi. Basi, mto ulipotokea na kupasua hapo, ilianguka papo hapo, kupasuka kwake ile nyumba kukawa kukubwa. Alipokwisha kuyasema maneno yake yote, watu wakimsikiliza, akaenda, akaingia Kapernaumu. Kukawako mkubwa wa askari mwenye mtumwa, ambaye alipendezwa sana naye; huyu alikuwa mgonjwa wa kufa. Bwana wake aliposikia mambo ya Yesu akatuma kwake wazee wa Wayuda, wamwombe, aje, amponye mtumwa wake. Walipomfikia Yesu wakakaza kumbembeleza wakisema: Amepaswa, umfanyie hivyo; kwani anatupenda sisi taifa letu, hata nyumba ya kuombea ametujengea mwenyewe. Yesu akaenda pamoja nao; alipokuwa mbali kidogo kuifikia ile nyumba, yule mkubwa wa askari akatuma rafiki zake kumwambia: Bwana, usijisumbue! Kwani hainipasi, uingie kijumbani mwangu. Kwa hiyo nami sikujipa moyo wa kukujia mwenyewe. Ila sema neno tu! ndipo, mtoto wangu atakapopona! Kwani nami ni mtu mwenye kuitii serikali, ninao askari chini yangu. Nami nikimwambia huyu: Nenda! basi, huenda; na mwingine: Njoo! huja; nikimwagiza mtumishi wangu: Vifanye hivi! huvifanya. Yesu alipoyasikia hayo akamstaajabu, akaligeukia kundi la watu lililomfuata, akasema: Nawaambiani, hata kwa Waisiraeli sijaona bado mwenye kunitegemea kama huyu. Wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa, yuko amepona. *Kisha punde kidogo akashika njia kwenda katika mji, jina lake Naini. Wakafuatana naye wanafunzi wake na kundi la watu wengi. Alipolikaribia lango la mji, panatolewa mfu; huyu alikuwa mwana wa pekee wa mama yake, naye alikuwa mjane. Kwa hiyo watu wengi wa mji ule walikwenda pamoja naye. Bwana alipomwona akamwonea uchungu, akamwambia: Usilie! Alipofika karibu, alishike jeneza, wachukuzi wakasimama. Akasema: Kijana, nakuambia: Inuka! Ndipo, yule mfu alipoinuka, akaanza kusema; kisha akampa mama yake. Woga ukawashika wote, wakamtukuza Mungu wakisema: Mfumbuaji mkuu ametutokea, naye Mungu amewakagua wao wa ukoo wake. Hili neno lake, alilolifanya, likaja kuenea Uyuda wote na nchi zote zilizoko pembenipembeni.* Wanafunzi wake walipomsimulia Yohana hayo yote, akaita wanafunzi wake wawili, akawatuma kwa Bwana, wamwulize: Wewe ndiwe mwenye kuja, au tungoje mwingine? Waume hao walipofika kwake wakasema: Yohana Mbatizaji ametutuma kwako, tuulize: Wewe ndiwe mwenye kuja, au tungoje mwingine? Saa ileile alikuwa akiponya wengi wenye magonjwa na maumivu na pepo wabaya; nao vipofu wengi akawapa kuona. Akajibu akiwaambia: Rudini, mmsimulie Yohana, mliyoyaona nayo mliyoyasikia: vipofu wanaona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanapigiwa mbiu njema. Tena mwenye shangwe ndiye asiyejikwaa kwangu. Wajumbe wa Yohana walipokwisha kwenda zao, akaanza kusema na yale makundi ya watu mambo ya Yohana: Mlipotoka kwenda nyikani mlikwenda kutazama nini? Mlikwenda kutazama utete unaotikiswa na upepo? Au mlitoka kutazama nini? Mlikwenda kutazama mtu aliyevaa mavazi mororo? Tazameni, wanaovaa mavazi yenye utukufu na kula vya mali wamo nyumbani mwa wafalme. Au mlitoka kutazama nini? Mlitaka kuona mfumbuaji? Kweli, nawaambiani: Ni mkuu kuliko mfumbuaji. Huyo ndiye aliyeandikiwa: Utaniona, nikimtuma mjumbe wangu, akutangulie, aitengeneze njia yako mbele yako. Nawaambiani: Miongoni mwao wote waliozaliwa na wanawake hakuna mkuu kuliko Yohana. Lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye. Watu wote waliomsikia, hata watoza kodi wakauitikia wongofu wake Mungu, wakabatizwa ubatizo wa Yohana. Lakini Mafariseo na wajuzi wa Maonyo waliyatengua, Mungu aliyoyataka, wayafanye, wasibatizwe naye. Basi, wao wa kizazi hiki niwafananishe na nini? Au wamefanana na mtu gani? Wamefanana na watoto wanaokaa sokoni na kuitana wao kwa wao wakisema: Tumewapigia filimbi, nanyi hamkucheza; tena tumewaombolezea, nanyi hamkulia. Kwani Yohana Mbatizaji alikuja, hakula mkate, wala hakunywa mvinyo, nanyi mkasema: Ana pepo. Mwana wa mtu amekuja, akala, akanywa, nanyi mkasema: Tazameni mtu huyu mlaji na mnywaji wa mvinyo, mpenda watoza kodi na wakosaji! Lakini werevu hutokezwa na watoto wake wote kuwa wa kweli. *Fariseo mmoja alipomwalika, ale pamoja naye, akaingia nyumbani mwa yule Fariseo, akakaa chakulani. Mjini mle mlikuwa na mwanamke mkosaji. Naye alipotambua, ya kuwa yumo mwa yule Fariseo, amekaa chakulani, akaja na kichupa cha manukato, akamsimamia nyuma miguuni pake mwenye machozi, akaanza kuyadondosha miguuni pake, akayasugua kwa nywele za kichwani pake, akainonea miguu yake, kisha akaipaka manukato. Yule Fariseo aliyemwalika alipoviona akasema moyoni mwake: Huyu kama angekuwa mfumbuaji, angemtambua mwanamke huyu anayemgusa, kama ni nani, kama ni wa namna gani, kwamba ni mkosaji. Yesu akajibu akimwambia: Simoni, ninalo la kukuambia. Naye alipomwambia: Mfunzi, sema! akasema: Mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili. Wa kwanza deni lake ni shilingi 500, mwenzake 50. Walipokosa vya kulipa, akawaachilia wote wawili, wasilipe. Katika hao atakayempenda kumpita mwenziwe ni yupi? Simoni akajibu akisema: Nadhani, ni yule aliyeachiliwa nyingi. Naye akamwambia: Ulivyolikata shauri hili, ndivyo kweli. Kisha akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni: Unamtazama mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu; lakini huyu alinidondoshea machozi miguuni pangu, akayasugua kwa nywele za kichwani pake. Hukuninonea, lakini huyu, tangu nilipoingia, hakuacha kuinonea miguu yangu. Wewe hukunipaka mafuta kichwani, lakini huyu ameipaka miguu yangu manukato. Kwa hiyo nakuambia: Ameondolewa makosa yake yaliyo mengi, kwani mapendo yake ni mengi. Lakini anayeondolewa machache tu, naye mapendo yake ni machache. Kisha akamwambia yule mwanamke: Wewe umeondolewa makosa yako. Ndipo, wale waliokaa chakulani pamoja naye walipoanza kusema mioyoni mwao: Huyu ni nani akiondoa hata makosa? Naye akamwambia yule mwanamke: Kunitegemea kwako kumekuokoa; nenda na kutengemana!* Kisha akatembea na kuingia mwenyewe mji kwa mji na kijiji kwa kijiji, akiutangaza Utume mwema wa ufalme wa Mungu nao wale kumi na wawili walikuwa pamoja naye, hata wanawake wengine waliokuwa wameponywa pepo wabaya na magonjwa; ndio Maria anayeitwa Magadalene aliyetokwa na pepo saba, na Yohana, mkewe Kuza aliyekuwa mshika mali wa Herode, na Susana na wengine wengi, wakawatumikia na kuwagawia, waliyokuwa nayo. *Lakini lilipokusanyika kundi la watu wengi na kumwendea toka kila mji, akasema kwa mfano: Mpanzi alitoka kuzimiaga mbegu zake. Ikawa, alipozimiaga, nyingine zikaangukia njiani, zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila. Nyingine zikaangukia mwambani, zikaota, mara zikanyauka, kwa kuwa hazina mchanga mbichi. Nyingine zikaangukia miibani katikati, nayo miiba ikaota pamoja nazo, ikazisonga. Nyingine zikaangukia penye mchanga mwema, zikaota, zikazaa punje mia. Alipoyasema haya akapaza sauti kwamba: Mwenye masikio yanayosikia na asikie! Wanafunzi wake walipomwuliza maana ya mfano huu, akasema: Ninyi mmepewa kuyatambua mafumbo ya ufalme wa Mungu, lakini wale wengine huambiwa kwa mifano, kusudi watazame, lakini wasione, wasikilize, lakini wasijue maana. Nao mfano maana yake ni hii: mbegu ndio Neno la Mungu. Zilizoko njiani ndio wenye kulisikia; kisha huja Msengenyaji, akaliondoa Neno mioyoni mwao, wasipate kulitegemea na kuokoka. Nazo zilizoko mwambani ndio hao: wanapolisikia Neno hulipokea kwa furaha, lakini hawana mizizi, hulitegemea kitambo kidogo, kisha siku za kujaribiwa hujitenga. Lakini zilizoangukia miibani ndio hao: wanalisikia, lakini huenda zao, Neno likisongwa nayo masumbuko na mali nyingi na furaha za ulimwenguni; hivyo hawaivishi punje. Lakini zilizoko penye mchanga mzuri ndio hao: wanalisikia Neno na kulishika katika mioyo iliyo mizuri na miema; ndio wanaozaa matunda kwa kuvumilia.* Hakuna mwenye kuwasha taa anayeifunika kwa chombo au anayeiweka mvunguni mwa kitanda; ila huiweka juu ya mwango, maana wanaoingia waone mwanga. Kwani hakuna ililofichwa lisiloonekana halafu; wala hakuna njama isiyotambulikana halafu na kutokea waziwazi. Basi, mwangalie, jinsi mnavyosikia! Kwani aliye na mali atapewa; lakini asiye na kitu atachukuliwa hata kile, alichokiwaza kuwa chake. Kisha mama yake na ndugu zake wakamjia, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya kundi la watu. Alipopashwa habari kwamba: Mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kuonana na wewe, akajibu akiwaambia: Mama yangu na ndugu zangu ndio hawa wanaolisikia Neno la Mungu na kulifanya. Ikawa siku moja, mwenyewe akajipakia chomboni na wanafunzi wake, akawaambia: Tuvuke kwenda ng'ambo ya ziwa! Wakatweka matanga. Walipoendelea baharini, akalala usingizi. Kukashuka msukosuko wa upepo ziwani, chombo kikajaa maji, wakafikisha kuangamia. Ndipo, walipomjia, wakamwamsha wakisema: Bwana, Bwana, tunaangamia! Naye alipoinuka, akaukaripia upepo na mawimbi ya maji, yakatulia, kukawa kimya. Kisha akawaambia: Tegemeo lenu liko wapi? Kwa kuogopa wakastaajabu tu, wakasemezana wao kwa wao: Ni mtu gani huyu, ya kuwa anaagiza hata upepo na maji, nayo yanamtii! Walipokwisha kuvuka, wakafika katika nchi ya Wagerasi iliyoelekea Galilea. Aliposhuka pwani akakutana na mwanamume wa mji ule aliyekuwa na pepo; huyo siku nyingi hakuvaa nguo, wala hakukaa nyumbani, ila hukaa penye makaburi. Alipomwona Yesu akapiga kelele, akamwangukia, akapaza sauti akisema: Tuko na jambo gani, mimi na wewe Yesu, Mwana wa Mungu Alioko huko juu? Nakuomba wewe, usiniumize. Kwani alikuwa amemwagiza yule pepo mchafu, amtoke yule mtu. Kwani mara nyingi alikuwa amemsukumasukuma, naye alikuwa amefungwa kwa minyororo na kwa mapingu na kulindwa, akavivunja vile vifungo, akakimbizwa na pepo kwenda mahali pasipo na watu. Yesu alipomwuliza: Jina lako nani? akasema: Maelfu. Kwani alikuwa ameingiwa na pepo wengi. Nao wakambembeleza, asiwaagize kwenda zao kuzimuni. Basi, kulikuwako kundi la nguruwe wengiwengi waliokuwako malishoni mlimani. Wakambembeleza, awape ruhusa ya kuwaingia wale. Alipowapa ruhusa, pepo wakamtoka yule mtu, wakawaingia nguruwe; ndipo, kundi lilipotelemka mbio mwambani, wakaingia ziwani, wakatoswa. Lakini wachungaji walipoliona lililofanyika, wakakimbia, wakalitangaza mjini na mashambani. Watu wakatoka kwenda kulitazama lililofanyika; walipofika kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyetokwa na pepo, anavyokaa miguuni pa Yesu, amevaa nguo, tena ana akili zake, wakashikwa na woga. Nao walioyaona wakawasimulia, mwenye pepo alivyoponywa. Kwa hiyo watu waliokuwa wengi katika nchi za pembenipembeni za Wagerasi wakamwomba wote, aondoke kwao, kwani walishikwa na woga mkubwa. Alipojipakia chomboni, arudi, yule mtu aliyetokwa na pepo akamwomba, afuatane naye. Lakini yeye akamwaga akisema: Rudi nyumbani mwako, ukayasimulie yote, Mungu aliyokutendea! Ndipo, alipokwenda zake, akayatangaza katika mji mzima yote, Yesu aliyomtendea. Yesu aliporudi, kundi la watu likampokea. Kwani wote walikuwa wakimngoja. Mara akaja mtu, jina lake Yairo; huyo alikuwa jumbe wa nyumba ya kuombea. Akamwangukia Yesu miguuni, akambembeleza, aje nyumbani mwake, kwani mwanawe wa kike wa pekee aliyekuwa mwenye miaka 12 aliingia kufani. Alipokwenda naye, watu wengi sana wakamsongasonga. Kukawa na mwanamke mwenye ugonjwa wa kutoka damu tangu miaka 12. Kwa kuwa hakuweza kuponywa na mtu ye yote, akamjia nyuma, akaligusa pindo la nguo yake. Papo hapo kijitojito cha damu yake kikakoma. Yesu akasema: Yuko nani aliyenigusa? Walipokana wote, Petero akasema: Bwana, makundi ya watu wanakusonga na kubanana. Yesu akasema: Yuko aliyenigusa, kwani nimetambua, jinsi nguvu ilivyonitoka. Yule mwanamke alipoona, ya kuwa hakufichika, akaja na kutetemeka, akamwangukia, akamweleza mbele ya watu wote sababu ya kumgusa na jinsi alivyopona papo hapo. Naye akamwambia: Mwanangu, kunitegemea kwako kumekuponya, nenda na kutengemana! Angali akisema, akaja mtu wa jumbe wa nyumba ya kuombea, akasema: Binti yako amekwisha kufa, usimsumbue mfunzi tena! Yesu alipoyasikia akamwambia: Usiogope nitegemea tu! Atapona. Alipoingia nyumbani hakumpa mtu ruhusa kuingia pamoja naye, ila Petero na Yohana na Yakobo na baba yake mwana na mama yake. Kwa kuwa wote waliomboleza na kumlilia, akasema: Msilie! kwani hakufa, ila amelala usingizi tu. Ndipo, walipomcheka sana, maana walijua, ya kuwa amekwisha kufa. Kisha akamshika mkono wake, akapaza sauti akisema: Mtoto, inuka! Papo hapo roho yake ikarudi, akafufuka; naye akawaagiza, apewe chakula. Wazazi wake washangaa. Naye akawakataza, wasimwambie mtu lililofanyika. Akawaita wale kumi na wawili, wakusanyike, akawapa uwezo na nguvu za kufukuza pepo wote na za kuponya magonjwa. Akawatuma, wautangaze ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. Akawaambia: Msichukue kitu cha njiani, wala fimbo wala mkoba wala chakula wala shilingi, tena mtu asiwe na nguo mbili! Nyumbani mo mote mtakamoingia, kaeni humo! Namo ndimo, mtakamotoka tena! Nao wote wasiowapokea, basi, utokeni mji wao na kuyakung'uta mavumbi yaliyoishika miguu yenu, yaje yanishuhudie kwao! Wakatoka, wakapita vijijini wakiipiga hiyo mbiu njema na kuponya wagonjwa po pote. Mfalme Herode alipoyasikia mambo yote yaliyokuwapo, akahangaika, maana wengine walisema: Yohana amefufuka katika wafu, wengine: Elia ametokea, wengine: Mmoja wao wafumbuaji wa kale amefufuka. Lakini Herode akasema: Yohana mimi nimemkata kichwa. Lakini huyo ni nani, ninayemsikia mambo kama hayo? Akatafuta kumwona. Mitume waliporudi, wakamsimulia mambo yote, waliyoyafanya. Kisha akawachukua, akaondoka kwenda nao peke yao, wakaingia mji, jina lake Beti-Saida. Makundi ya watu walipovitambua wakamfuata, naye akawapokea, akasema nao mambo ya ufalme wa Mungu, akawaponya waliopaswa na kuponywa. Jua lilipotaka kuchwa, wale kumi na wawili wakamjia, wakamwambia: Uliage kundi la watu, waende zao vijijini na mashambani huko pembenipembeni, waone ulalo na vyakula, kwani hapa tulipo ni nyika. Akawaambia: Wapeni ninyi vyakula! Wakasema: Sisi hatuna kitu hapa kuliko mikate mitano na visamaki viwili; au twende sisi kuwanunulia watu hawa wote vyakula? Kwani waume tu waliokuwako walipata 5000. Akawaambia wanafunzi wake: Mwaagize, wakae mafungumafungu kama hamsinihamsini! Wakafanya hivyo, wakawakalisha wote. Akaitwaa ile mikate mitano na vile visamaki viwili, akatazama juu mbinguni, akaviombea, akawamegeamegea, akawapa wanafuanzi, wawapangie hao watu wengi. Wakala, wakashiba wote, pakaokotwa makombo yaliyowasalia vikapu kumi na viwili. *Ikawa, alipokuwa akiomba peke yake, wakawapo pamoja naye wanafunzi wake, akawauliza akisema: Makundi ya watu hunisema kuwa ni nani? Nao wakajibu wakisema: Wanakusema kuwa u Yohana Mbatizaji, wengine: Elia, wengine husema: Amefufuka mmoja wao wafumbuaji wa kale. Kisha akawauliza: Lakini ninyi mnanisema kuwa ni nani? Petero akajibu akisema: Kristo wa Mungu. Ndipo, alipowatisha na kuwakataza, wasimwambie mtu neno hilo. Akawaambia: Imempasa Mwana wa mtu kutwa mengi na kukataliwa nao wazee na watambikaji wakuu na waandishi, mpaka auawe, kisha afufuliwe siku ya tatu. Akawaambia wote: Mtu akitaka kunifuata mimi ajikataze mapenzi yake, ajitwishe kila siku nao msalaba wake, kisha anifuate! Maana mtu anayetaka kuiokoa roho yake ataiangamiza. Lakini mtu atakayeiangamiza roho yake kwa ajili yangu mimi, huyo ataiokoa. Kwani mtu vinamfaa nini, avichume vya ulimwengu wote, akijiangamiza mwenyewe, au akiponzwa navyo? Kwani mtu atakayenionea soni mimi na maneno yangu, basi, naye Mwana wa mtu atamwonea soni huyo atakapokuja mwenye utukufu wake yeye na wa Baba yake na wa malaika watakatifu.* Lakini nawaambiani lililo kweli: Miongoni mwao wanaosimama hapa wamo wengine, ambao hawatakuonja kufa, mpaka watakapouona ufalme wa Mungu. Ikawa, walipokwisha kuyasema hayo, zikipita kama siku nane, akamchukua Petero na Yohana na Yakobo, wakapanda mlimani kuomba Alipokuwa akiomba, sura ya uso wake ikawa nyingine, nazo nguo zake zikawa nyeupe na kumerimeta. Walipotazama, wakawako waume wawili wakiongea naye, nao walikuwa Mose na Elia. Wakawatokea wenye utukufu, wakasema naye, ndivyo aende kuyatimiza mambo ya kufa kwake kule Yerusalemu. Lakini Petero na wenziwe walikuwa wamelemewa na usingizi. Walipoamka wakauona utukufu wake na wale waume wawili waliosimama naye. Ikawa, walipotengwa naye, Petero akamwambia Yesu: Bwana, hapa ni pazuri kuwapo sisi, na tujenge vibanda vitatu, kimoja chako, na kimoja cha Mose, na kimoja cha Elia! kwani hakujua, alilolisema. Angali akiyasema haya, pakawa na wingu, likawatia kivuli, wakashikwa na woga walipoingiwa na wingu lile. Sauti ikatoka winguni, ikasema: Huyu ndiye mwanangu, niliyemchagua, msikilizeni yeye! Sauti hiyo iliposikilika, Yesu akaonekana, yuko peke yake. Siku zile wakanyamaza, wasimsimulie mtu hata moja lao hayo waliyoyaona. Ikawa siku ya kesho, waliposhuka mlimani wakakutana na kundi la watu wengi. Mle kundini mkawamo mwanamume, akapaza sauti akisema: Mfunzi, nakuomba, umtazame huyu mwanangu, kwani ni wangu wa pekee! Tazama, pepo humpagaa, naye mara moja hulia kwa kukumbwa, mpaka akitoka pofu; akiisha kumlegeza hukawia kumwondokea. Nikawaomba wanafunzi wako, wamfukuze, lakini hawakuweza. Yesu akajibu akisema: Enyi wa kizazi kisichomtegemea Mungu kwa kupotoka! Nitakuwapo nanyi na kuwavumilia mpaka lini? Umlete mwana wako, aje hapa! Alipokuwa akija, pepo akamkamata kwa nguvu, akamkumba. Lakini Yesu akamkaripia huyo pepo mchafu, akamponya mtoto, akamrudishia baba yake. Ndipo, wote walipoingiwa na kituko kwa ajili ya ukubwa wa nguvu yake Mungu. Wao wote walipoyastaajabu yote, aliyoyafanyiza, akawaambia wanafunzi wake: Myaweke vema maneno haya masikioni mwenu! Maana Mwana wa mtu atatiwa mikononi mwa watu. Lakini hawakulitambua neno hili, likawa limefichiwa wao, wasilione maana. Nao wakaogopa kumwuliza tena neno hilo. Wakawa wakiwaza mioyoni mwao kwamba: Aliye mkuu kwetu ni nani? Lakini Yesu akayajua, waliyoyawaza mioyoni mwao, akatwaa kitoto, akamsimamisha kando yake, akawaambia: Mtu atakayempokea kitoto huyu kwa Jina langu hunipokea mimi. Tena akinipokea mimi humpokea yule aliyenituma mimi. Kwani aliye mdogo kwenu ninyi wote, huyo ndiye mkuu. Yohana akajibu akisema: Bwana, tuliona mtu anayefukuza pepo kwa Jina lako; tukamzuia, kwani hafuatani nasi. Yesu akamwambia: Msimzuie! Kwani asiyewakataa yuko upande wenu. *Ikawa, zilipotimia siku zake za kuchukuliwa mbinguni, mwenyewe akauelekeza uso kwenda Yerusalemu, akatanguliza wajumbe mbele yake. Hao walipokwenda, kuingia kijiji cha Wasamaria, wamtengenezee mahali, hawakumpokea, kwani uso wake ulikuwa umeelekea kwenda Yerusalemu. Wanafunzi akina Yakobo na Yohana walipoviona wakasema: Bwana, wataka, tuseme, moto ushuke toka mbinguni, uwamalize, kama Elia naye alivyofanya? Lakini akapinduka, akawatisha akiwaambia: Hamjui, kama m wenye Roho gani? Mwana wa mtu hakujia kuangamiza roho za watu, ila kuziokoa. Kisha wakaenda zao, wakafikia kijiji kingine.* Walipokuwa wakienda njiani, palikuwapo aliyemwambia: Nitakufuata po pote, utakapokwenda. Yesu akamwambia: Mbweha wanayo mapango, nao ndege wa angani wanavyo vituo, lakini Mwana wa mtu hana pa kukilazia kichwa chake. Alipomwambia mtu mwingine akasema: Nifuate! huyo akasema: Nipe ruhusa, kwanza niende nimzike baba yangu! Naye akamwambia: Waache wafu, wazike wao kwa wao! Lakini wewe nenda, uutangaze ufalme wa Mungu! Mtu mwingine akasema: Nitakufuata, Bwana, lakini kwanza nipe ruhusa, niwaage waliomo nyumbani mwangu! Yesu akamwambia: Mtu ashikaye jembe mkononi na kuvitazama vya nyumba, huyo hatauweza ufalme wa Mungu.* Kisha Bwana akachagua wengine 70, akawatanguliza mbele yake wawiliwawili, waingie kila mji na kila mahali, alipotaka kwenda mwenyewe. Naye akawaambia: Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Mwombeni mwenye mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake! Nendeni! Tazameni, nawatuma ninyi, mwe kama wana kondoo walio katikati ya mbwa wa mwitu! Msitwae mfuko wala mkoba wala viatu! Tena msiamkiane na mtu njiani! Lakini nyumbani mo mote, mtakamoingia, kwanza semine: Nyumba hii itengemane! Itakapokuwa, yumo mwenye kutengemana, utengemano wenu utamkalia. Lakini kama hatakuwamo, utawarudia ninyi. Namo nyumbani mlemle mkaeni mkila, mkinywa mnavyopewa! Kwani mtenda kazi hupaswa na kupewa mshahara wake. Msizunguke nyumba kwa nyumba! Namo mjini mo mote, mtakamoingia, nao wakiwapokea, vileni, mnavyoandaliwa! Waponyeni wagonjwa waliomo nakuwaambia: Ufalme wa Mungu umewakaribia! Lakini mjini mo mote, mtakamoingia, wasipowapokea, tokeni Lakini mjini mo mote, mtakamoingia, wasipowapokea, tokeni mwao, mwende uwanjani mkisema: Hata mavumbi ya mji wenu yaliyotushika miguuni twawakung'utia ninyi; lakini haya yatambueni: Ufalme wa Mungu umekaribia! Nawaambiani: Siku ile mji wa Sodomu utapata mepesi kuliko mji ule. Yatakupata, wewe Korasini! Yatakupata, wewe Beti-Saida! Kwani ya nguvu yaliyofanyika kwenu kama yangalifanyika Tiro na Sidoni, wangalijuta kale na kujivika magunia na kujikalisha majivuni. Lakini penye hukumu miji ya Tiro na Sidoni itapata machungu yaliyoi madogo kuliko yenu. Nawe Kapernaumu, hukupazwa mpaka mbinguni? Utatumbukia mpaka kuzimuni. Anayewasikia ninyi hunisikia mimi. Naye anayewatengua ninyi hunitengua mimi. Naye anayenitengua mimi humtengua naye aliyenituma. *Wale 70 wakarudi wenye furaha, wakasema: Bwana, hata pepo hututii kwa Jina lako. Ndipo, alipowaambia: Nalimwona Satani, akianguka kama umeme toka mbinguni. Tazameni, nimewapa nguvu za kukanyaga nyoka na nge, mshinde uwezo wote wa yule mchukivu, tena hakuna kitu kitakachowapotoa. Lakini msiyafurahie hayo, ya kuwa pepo huwatii, ila yafurahieni, ya kuwa mmeandikwa majina yenu mbinguni!* Saa ileile Roho Mtakatifu akamshangiliza, naye akasema: Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwani hayo umewaficha werevu na watambuzi, ukawafunulia wachanga. Ndio, Baba, kwani hivyo ndivyo, ulivyopendezwa navyo. Vyote nimepewa na Baba yangu. Hakuna anayemtumbua Mwana, kama ni nani, pasipo Baba; wala hakuna anayemtambua Baba, kama ni nani, pasipo Mwana, na kila, Mwana atakayemfunulia. *Akawapindukia wanafunzi, akawaambia, walipokuwa peke dyao: Yenye shangwe ni macho yanayoyaona, mnayoyaona ninyi. Kwani nawaambiani: Wengi waliokuwa wafumbuaji na wafalme walitaka kuyaona, mnayoyaona ninyi, lakini hawakuyaona; walitaka kuyasikia, mnayoyasikia ninyi, lakini hawakuyasikia. Pakawapo mjuzi wa Maonyo, akainuka, akamtega akisema: Mfunzi, nifanye nini, nipate kuurithi uzima wa kale na kale? Naye akamwambia: Katika Maonyo imeandikwa nini? Unasomaje? Akajibu akisema: Umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa nguvu yako yote na kwa mawazo yako yote! Naye mwenzio umpende, kama unavyojipenda mwenyewe! Akamwambia: Umejibu kweli; yafanye hayo! Ndipo, utakapopata kuishi. Lakini kwa sababu alitaka kujijulisha kuwa ni mwongofu, akamwambia Yesu: Mwenzangu ni nani? Yesu akalishika neno hili akisema: Kulikuwa na mtu, alitoka Yerusalemu, akatelemka kwenda Yeriko, akaguiwa na wanyang'anyi. Hao walipokwisha kumvua nguo zake, na kumpiga vigongo, wakaenda zao na kumwacha, akitaka kufa. Ikatukia, mtambikaji akiitelemkia njia ile; alipomwona akaepuka, akapita. Vilevile hata Mlawi akafika mahali pale; lakini alipomwona akaepuka, akapita. Kisha Msamaria aliyeifuata njia ile akaja huko, alikokuwa; alipomwona akamwonea uchungu, akamjia, akamfunga madonda yake akiyamwagia mafuta na mvinyo, akampandisha juu ya punda wake yeye mwenyewe, akampeleka kifikioni, akamwuguza. Siku ya kesho akatoa shilingi mbili, akampa mwenye fikio, akasema: Mwuguze huyu! Kama unatumia kuzipita hizi, nitakulipa zote nitakaporudi. Waonaje? Katika hao watatu aliyejifanya kuwa mwenzake yule aliyeguiwa na wanyang'anyi ni yupi? Naye akasema: Ndiye aliyemwonea huruma. Ndipo, Yesu alipomwambia: Nenda nawe, ufanye vivyo hivyo!* *Walipokwenda zao, akaingia kijijini. Mlikuwa na mwanamke, jina lake Marta, akamfikiza nyumbani mwake. Naye alikuwa na ndugu yake aliyeitwa Maria; huyu akajiketisha miguuni pa Bwana, akamsikiliza maneno yake. Lakini Marta akabururwa huko na huko kwa utumikizi mwingi. Kisha akaja kusimama hapo, alipokuwa, akasema: Bwana, huvitazami, huyu ndugu yangu akiniacha, nitumike peke yangu? Umwambie, anisaidie! Lakini Bwana akajibu akimwambia: Marta, Marta, unahangaika kwa kusumbukia mambo mengi. Lakini vinavyopasa ni vichache au kimoja tu. Maria amelichagua fungu lililo jema, naye hatapokwa.* Ikawa alipokuwa mahali akiomba, akiisha, mwanafunzi wake mmoja akamwambia: Bwana, tufundishe hata sisi kuomba, kama naye Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake! Akawaambia: Mnapoomba semeni: Baba yetu ulioko mbinguni, Jina lako litakaswe! Ufalme wako uje! Uyatakayo yatimizwe nchini, kama yanavyotimizwa mbinguni! Tupe kila siku chakula chetu cha kututunza! Tuondolee makosa yetu! Kwani nasi wenyewe humwondolea kila aliyetukosea. Usituingize majaribuni! Ila tuokoe maovuni! *Akawaambia: Kulikuwa na mtu mwenye rafiki; huyu akamwendea usiku wa manane na kumwambia: Rafiki yangu, unikopeshe mikate mitatu! Kwani rafiki yangu aliyechwelewa njiani amenifikia, nami sina cha kumwandalia. Basi, kwenu yule wa ndani atamjibu nini? Atamwambia: Usinisumbue! Kwani mlango umekwisha fungwa, nao watoto wangu wako kitandani pamoja nami; siwezi kuinuka, nikupe? Nawaambiani: Ijapo, asiinuke, ampe, kwa sababu ni rafiki yake, lakini atainuka, ampe yote yampasayo ya mgeni, kwa sababu hana soni ya kuomba. Nami nawaambiani: Ombeni! ndipo, mtakapopewa. Tafuteni! ndipo, mtakapoona. Pigeni hodi! ndipo, mtakapofunguliwa mlango. Kwani kila anayeomba hupewa, naye anayetafuta huona, naye anayepiga hodi hufunguliwa mlango. Tena kwenu yuko baba, mwanawe anapomwomba samaki, ampe nyoka, asimpe samaki? Au anapomwomba yai, ampe nge? Basi, ninyi mlio wabaya mkijua kuwapa watoto wenu vipaji vyema, Baba alioko mbinguni asizidi kuwapa Roho Mtakatifu wanaomwomba?* *Akawa akifukuza pepo aliyekuwa bubu; naye pepo alipotoka, bubu akaanza kusema. Ndipo, makundi ya watu walipostaajabu. Lakini walikuwako waliosema: Nguvu ya Belzebuli, mkuu wa pepo, ndiyo, anayofukuzia pepo. Wengine wakamjaribu wakitaka, afanye kielekezo kitokacho mbinguni. Kwa kuyajua hayo mawazo yao, akawaambia: Kila ufalme unapogombana wao kwa wao huwa mahame tu, nazo nyumba huangukiana. Naye Satani anapojigombanisha mwenyewe, ufalme wake utasimamikaje? Kwani mnasema: Nafukuza pepo kwa nguvu ya Belzebuli. Nami nikiwafukuza pepo kwa nguvu ya Belzebuli, Je? Wana wenu huwafukuza kwa nguvu ya nani? Kwa hiyo hao ndio watakaowaumbua. Lakini mimi nikiwafukuza pepo kwa nguvu ya kidole cha Mungu, ufalme wa Mungu umekwisha kuwafikia ninyi. Mwenye nguvu akililinda boma lake na kushika mata, basi, yaliyo yake yatakaa na kutengemana. Lakini mwenye nguvu kuliko yeye atakapomjia na kumshinda atamnyang'anya mata yake yote yaliyomshikiza, kisha atayagawanya mateka. Asiye wa upande wangu hunikataa; naye asiyekusanya pamoja nami hutapanya., Pepo mchafu anapomtoka mtu hupita mahali pasipo na maji akitafuta kituo. Asipokiona husema: Nitarudi nyumbani mwangu, nilimotoka. Anapokuja huiona, imefagiwa na kupambwa. Ndipo, anapokwenda kuchukua pepo saba wengine walio wabaya kuliko yeye; nao huingia, wakae humo: hivyo ya mwisho ya mtu yule yatakuwa mabaya kuliko ya kwanza. Ikawa, alipoyasema haya, mwanamke aliyekuwako katika kundi la watu akapaza sauti akimwambia: Lenye shangwe ni tumbo lililokuzaa na maziwa, uliyoyanyonya. Naye akasema: Kweli wenye shangwe ndio wanaolisikia Neno la Mungu na kulishika.* Makundi ya watu walipomkusanyikia, akaanza kusema: Ukoo huu ni ukoo mbaya; wanatafuta kielekezo, lakini hawatapata kielekezo, ila kielekezo cha Yona. Kwani kama Yona alivyowawia watu wa Niniwe kielekezo, ndivyo naye Mwana wa mtu atakavyowawia wao wa ukoo huu kielekezo. Yule mfalme wa kike aliyetoka kusini atawainukia waume wa ukoo huu siku ya hukumu, awaumbue. Kwani yeye alitoka mapeoni kwa nchi, aje kuusikia werevu wa Salomo uliokuwa wa kweli. Tena tazameni, hapa yupo anayempita Salomo! Siku ya hukumu waume wa Niniwe watauinukia ukoo huu, wauumbue; kwani walijuta kwa tangazo la Yona. Tena tazameni, hapa yupo anayempita Yona! Hakuna mwenye kuwasha taa anayeiweka panapofichika au chini ya kapu, ila huiweka juu ya mwango, maana wanaoingia waone mwanga. Taa ya mwili ni jicho lako. Basi, jicho lako liking'aa, nao mwili wako wote unao mwanga. Lakini likiwa bovu, nao mwili wako unayo giza. Kwa hiyo angalia, mwanga uliomo ndani yako usiwe giza! Mwili wako unapokuwa wote unao mwanga, pasiwe upande wenye giza, ndipo, utakapokuwa na mwanga pia, utakuwa kama taa inayokumulikia mwanga wa umeme. Alipokuwa katika kusema, Fariseo akamwalika chakulani. Naye akaingia, akakaa mezani. Fariseo huyo alipoviona akastaajabu, ya kuwa hakunawa kwanza kabla ya kula. Bwana akamwambia: Ninyi Mafariseo, vinyweo na vyano mnaviosha nje, lakini ndani ninyi mmejaa mapokonyo na mabaya. M wajinga, aliyevifanya vya nje hakuvifanya vya ndani navyo? Basi, vile vilivyomo ndani vigawieni watu! Mara vyenu vyote huwa safi. Yatawapata, ninyi Mafariseo, kwani fungu la kumi mnalitolea hata mchicha na nyanya na mboga zo zote. Lakini penye hukumu napo penye upendo wa Mungu mnapapita. Haya yawapasa kuyashika pasipo kuyaacha yale. Yatawapata, ninyi Mafariseo, kwani nyumbani mwa kuombea mnapenda viti vya mbele, tena hupenda kuamkiwa na watu sokoni. Yatawapata, ninyi waandishi na Mafariseo, kwani mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu hukanyaga juu yao, wasiyajue. Ndipo, mjuzi wa Maonyo alipojibu akimwambia: Mfunzi, ukisema hayo unatutukana hata sisi. Naye akasema: Nanyi wajuzi wa Maonyo yatawapata, kwani mnatwika watu mizigo isiyochukulika, nanyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kidole chenu kimoja tu. Yatawapata ninyi, kwani mnayajenga makaburi ya wafumbuaji, nao baba zenu ndio waliowaua. Hivyo mnayashuhudia matendo ya baba zenu, ya kuwa yanawapendeza; kwani wale waliwaua, nanyi mnawajengea. Kwa sababu hii ujuzi wa Mungu ulisema: Nitatuma kwao wafumbuaji na mitume, wengine wao watawaua, wengine watawafukuza, wao wa kizazi hiki walipishwe damu za wafuambji wote zilizomwagwa tangu hapo, ulimwengu ulipoumbwa, kuanzia damu ya Abeli mpaka kuifikia damu ya Zakaria aliyeuawa katikati ya meza ya Bwana na Nyumba ya Mungu. Kweli nawaambiani: Wao wa kizazi hiki watazilipa. Yatawapata, ninyi wajuzi wa Maonyo, kwani mliutwaa ufunguo wa utambuzi; wenyewe hamkuingia, mkawazuia wao waliotaka kuingia. Alipotoka mle, waandishi na Mafariseo wakaanza kumtunduia sana na kumwuliza maneno mengi na kumnyatia wakiwinda maneno, anayoyasema, kama wataona la kumsuta. Makundi yalipokuwa yamekusanyika maelfu ya watu wakakanyagana kwa kuwa wengi; ndipo, alipoanza kuwaambia kwanza wanafunzi wake; Jilindeni kwa ajili ya chachu ya Mafariseo iliyo ujanja! Hakuna lililofunikwa lisilofunuliwa halafu, wala hakuna lililofichwa lisilotambulikana halafu. Maneno yote, mnayoyasema gizani, yatasikiwa mwangani; nalo mnalolinong'oneza masikioni nyumbani, litatangazwa barazani. Lakini nawaambiani ninyi, wapenzi wangu: Msiwaogope wanaoweza kuiua miili tu, kisha hawana wanachoweza kuwafanyia tena! Lakini nitawaonyeshani ninyi wa kumwogopa: Mwogopeni yule anayeweza kuwaua, kisha yuko na nguvu ya kuwatupa shimoni mwa moto! Kweli nawaambiani: Huyo mwogopeni! Je? Videge vitano haviuzwi kwa senti mbili? Lakini hata mmoja wao hasahauliwi mbele ya Mungu. Lakini kwenu ninyi hata nywele za vichwani penu zimehesabiwa zote. Kwa hiyo msiogope, ninyi mnapita videge vingi! Lakini nawaambiani: Kila atakayeungama mbele ya watu, kwamba ni mtu wangu, naye Mwana wa mtu ataungama mbele ya malaika wa Mungu, kwamba ni mtu wangu. Lakini atakayenikana mbele ya watu atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. Kila atakayesema neno la kumbisha Mwana wa mtu ataondolewa; lakini aliyembeza Roho Mtakatifu hataondolewa. Lakini watakapowapeleka katika nyumba za kuombea na mabomani na pengine penye nguvu msihangaikie wala mizungu wala maneno ya kujikania wala ya kuwajibu! Kwani Roho Mtakatifu atawafundisha saa ileile yapasayo kusema. Kundini mwa watu alikuwamo aliyemwambia: Mfunzi, umwambie ndugu yangu, agawanye nami urithi, baba aliotuachia! Naye akamwambia: Mwenzangu, yuko nani aliyeniweka, niwaamue na kuwagawanyia mali zenu? *Akawaambia: Tazameni, mjilinde kwa ajili ya choyo cho chote! Kwani mali zikiwa nyingi sizo zinazomweka mtu, akizishika. Akawaambia mfano akisema: Kulikuwa na mtu mwenye mali, ambaye shamba lake lilikuwa limezaa sana. Ndipo, alipofikiri moyoni mwake akisema: Nifanyeje? Kwani sina pa kuyawekea mavuno yangu? Kisha akasema: Nitafanya hivyo: nitayavunja mawekeo yangu, nijenge makubwa kuyapita hayo ndimo niziweke ngano zangu na mali zangu zote. Ndipo, nitakapoiambia roho yangu: Roho yangu, unayo mema mengi yaliyowekwa ya miaka mingi. Basi, tulia, ule, unywe na kuchangamka! Lakini Mungu akamwambia: Mpumbavu wee! Usiku huu watakutoza roho yako; nayo, uliyoyalimbika, yatakuwa ya nani? Ndivyo, vinavyoendelea vya mwenye kukusanya mali nyingi, asipoziweka kwa Mungu.* Akawaambia wanafunzi wake: Kwa hiyo nawaambiani: Msiyasumbukie maisha yenu mkisema: Tutakula nini? Wala msiisumbukie miili yenu mkisema: Tutavaa nini? Kwani maisha hupita vyakula, nao mwili hupita mavazi. Jifundisheni kwa makunguru! Hawapandi, wala hawavuni, wala hawana vichanja wala wekeo jingine. Naye Mungu anawalisha nao. Je? Ninyi hamwapiti ndege pakubwa? Tena kwenu yuko nani anayeweza kwa kusumbuka kwake kujiongezea miaka yake kipande kama cha mkono tu? Basi, msipokiweza hata kilicho kidogo sana, yale mengine mwayasumbukiaje? Jifundisheni kwa maua ya uwago, kama yanavyokua! Hayafanyi kazi wala hayafumi nguo. Lakini nawaambiani: Hata Salomo katika utukufu wake wote hakuvikwa kama moja lao. Basi, Mungu akiyavika hivyo majani ya porini yanayokaa leo tu, kesho yatupwe katika mabiwi, yateketee, je? Hatazidi kuwavika ninyi? Mbona mnamtegemea kidogo tu? Basi, ninyi msiulize: Tutakula nini? au: Tutakunywa nini? Wala msijikweze! Kwani wamizimu waliomo ulimwenguni ndio wanaoyatafuta hayo yote; lakini Baba yenu amewajua, ya kuwa mnapaswa nayo. Lakini utafuteni ufalme wake! Ndivyo mtakavyopewa hayo. Msiogope, mlio kikundi kidogo! Kwani baba yenu imempendeza kuwapa ninyi huo ufalme. Uzeni vitu vyenu, mpate ya kuwagawia maskini! Jishoneeni mifuko isiyochakaa ya kuwekea mbinguni limbiko lisilopungua! Tena ndiko, kusikofika mwizi, wala kusikoharibiwa na mende. Kwani limbiko lenu liliko, ndiko, nayo mioyo yenu itakakokuwa. *Mwe mmejifunga viuno vyenu, nazo taa zenu ziwe zinawaka! Nanyi mfanane na watu wanomngoja bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, kusudi wamfungulie mlango papo hapo, atakaporudi na kupiga hodi. Wenye shangwe ni watumwa wale, ambao bwana atakapokuja atawakuta, wakikesha. Kweli nawaambiani: Atajifunga na kuwaketisha chakulani, naye atakuja kuwatumikia. Wenye shangwe ndio, atakaowakuta hivyo, hata akija zamu ya pili au ya tatu ya kulinda usiku. Lakini litambueni neno hili: kama mwenye nyumba angaliijua saa, mwizi atakayojia, hangaliacha, nyumba yake ibomeolewe. Nanyi mwe tayari! Kwani Mwana wa mtu atajia saa, msiyomwazia. Petero akasema: Bwana, mfano huu unatuambia sisi tu au watu wote? Bwana akasema: Basi, yuko nani aliye mtunzaji mwelekevu na mwerevu, bwana wake atakayempa kuwatunza watumwa wake, awape posho, saa yao itakapofika? Mwenye shangwe ni mtumwa yule, bwana wake atakayemkuta, akifanya hivyo, atakapokuja.* Kweli nawaambiani: Atampa kuzitunza mali zake zote. Lakini yule mtumwa akisema moyoni mwake: Bwana wangu anakawia, akaanza kuwapiga watumwa na vijakazi, hata kula na kunywa na kulewa, bwana wake mtumwa yule atamjia siku, asiyomngojea, na saa, asiyoitambua, kisha atamchangua kuwa vipande viwili, nalo fungu lake atampa pamoja nao wasiomtegemea Mungu. Maana yule mtumwa aliyeyatambua, bwana wake ayatakayo, asijitengeneze, wala asiyafanye hayo, aliyoyataka, huyo atapigwa fimbo nyingi. Lakini yule asiyeyatambua alipofanya yapasayo kupigwa atapigwa fimbo chache. Kwani kila aliyepewa mengi, kwake yatatafutwa mengi, naye waliyemwagizia mengi watazidi kumwuliza mengi. Nalijia kutupa moto nchini, tena hakuna ninachokitaka, ila uwake. Lakini ninao ubatizo, ndio nibatizwe; nami ninasongeka sana, mpaka umalizike. Mwaniwazia, kwamba nimejia kuiletea nchi utengemano? Nawaambiani: Sivyo, ila naleta matengano. Kwani tokea sasa watu watano waliomo katika nyumba moja watatengana, watatu wagombanishe wawili, nao wawili wagombanishe watatu. Watagombana baba na mwana wake, tena mwana na baba yake, tena mama na mwana wake wa kike, tena mwana wa kike na mama yake, vilevile mkwe na mkwewe. Akayaambia makundi ya watu: Mnapoona wingu linalotoka machweoni, papo hapo mnasema: Mvua inakuja; nayo inakuja kweli. Tena mnaposikia upepo unaovuma kusini mnasema: Litakuwa jua kali; nalo linakuwapo. Enyi wajanja, mnayoyaona ya nchini na ya mbinguni mnajua kuyapambanua, mbona hamzipambanui siku hizi za sasa? Tena ninyi wenyewe, mbona hamfuati uamuzi wenye wongofu? Kwani mnapokwenda bomani, wewe na mshitaki wako, umkaze njiani, mpatane, maana asikukokote kwa mwenye hukumu, naye mwenye hukumu asikutie mkononi mwa mpiga fimbo, naye mpiga fimbo asikutie kifungoni. Nakuambia: Hutatoka humo kabisa, mpaka utakapomaliza kulipa, isisalie hata senti moja. *Siku zilezile walikuwapo watu waliomsimulia ya Wagalilea, ambao Pilato alimwaga damu zao na kuzichanganya na damu za ng'ombe zao za tambiko. Akajibu akiwaambia: Mwadhani, Wagalilea hao walikuwa wakosaji kuwapita Wagalilea wote, maana wameteswa hivyo? Nawaambiani: Sivyo, ila msipojuta nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, uliowaangukia mnara kule Siloa na kuwaua, je? Mwadhani, wamekuwa wenye kulipizwa kuwapita wenyeji wote wa Yerusalemu? Nawaambiani: Sivyo, ila msipojuta nyote mtaangamia vivyo hivyo. Akausema mfano huu: Mtu alikuwa na mkuyu uliopandwa mizabibuni kwake. Alipokuja kutafuta matunda yake hakuyaona. Kisha akamwambia mlimia mizabibu: Tazama, imepita miaka mitatu, tangu nilipoanza kuja kutafuta matunda ya mkuyu huu, lakini siyaoni. Basi, uukate! Hulizuiliani shamba? Lakini huyo akajibu akimwambia: Bwana, uuache mwaka huu tu, niuchimbie pembenipembeni, nikautilie mbolea! Labda utazaa matunda siku zitakazokuja. Lakini usipozaa, basi, utaukata.* Akawa akifundisha siku ya mapumziko katika nyumba moja ya kuombea. Mle nyumbani mkawa na mwanamke mwenye pepo aliyemwuguza miaka 18; kwa hiyo alikuwa amepindana, asiweze kunyoka kamwe. Yesu alipomwona akamwita, akamwambia: Mama, umefunguliwa huu unyonge wako; Kisha akambandikia mikono yake. Papo hapo akanyoka, akamtukuza Mungu. Lakini mkuu wa nyumba ya kuombea akamkasirikia Yesu, kwa sababu amemponya siku ya mapumziko, akawaambia watu waliokuwamo: Ziko siku sita za kufanya kazi; basi, mje siku hizo, mpate kuponywa, lakini msiponywe siku ya mapumziko! Bwana akajibu akisema: Enyi wajanja, ninyi nyote hamwafungui ng'ombe au punda wenu zizini siku ya mapumziko na kuwapeleka, wanywe? Lakini huyu aliye mwana wa Aburahamu haikumpasa kufunguliwa siku ya mapumziko kifungo hiki, Satani alichomfunga miaka 18? Aliposema hayo, wabishi wake wakapatwa na soni wote, lakini wale watu wengi wote wakayafurahia mambo matukufu yote, aliyoyafanya. Kisha akasema: Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Niufananishe na nini? Umefanana na kipunje cha haradali, alichokitwaa mtu na kukitupia shambani kwake. Nacho hukua na kupata kuwa mti, hata ndege wa angani hutua katika matawi yake. Tena akasema: Ufalme wa Mungu niufananishe na nini? Umefanana na chachu, mwanamke akiitwaa, akaichanganya na pishi tatu za unga, mpaka ukachachwa wote. Naye alipofanya mwendo wa kwenda Yerusalemu akapita mijini na vijijini akiwafundisha. Mtu alipomwuliza: Bwana, watu watakaookoka ni wachache tu? akamwambia: Gombeeni, mpate kuuingia mlango ulio mfinyu! Nawaambiani: Wengi watataka kuuingia, lakini hawataweza. Tangu hapo, mwenye nyumba atakapoinuka na kuufunga mlango, ndipo, mtakapoanza kusimama nje na kuugonga mlango mkisema: Bwana, Bwana, tufungulie! Naye atajibu akiwaambia: Siwajui ninyi, mtokako. Ndipo, mtakapoanza kusema: Tumekula, tumekunywa machoni pako, nawe umetufundisha viwanjani petu. Ndipo, atakapowaambia ninyi: Siwajui, mtokako, ondokeni kwangu nyote mfanyao mapotovu! Ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno, mtakapowaona akina Aburahamu na Isaka na Yakobo na wafumbuaji wote, wamo katika ufalme wa Mungu, lakini ninyi wenyewe mtajiona, mmetupwa nje. Wako watakaotoka maawioni na machweoni kwa jua na upande wa kaskazini na wa kusini, nao watakaa chakulani katika ufalme wa Mungu. Tazameni, wako wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, tena wako wa kwanza watakaokuwa wa mwisho. Saa ileile wakawako Mafariseo waliomjia, wakamwambia: Toka hapa, ujiendee! kwani Herode anataka kukuua. Akawaambia: Nendeni, mkamwambie mbweha huyo: Tazama, leo na kesho nafukuza pepo na kuponya wagonjwa, nayo siku ya tatu mambo yangu yatamalizika. Lakini leo na kesho na kesho kutwa sharti niende, kwani haiwezekani, mfumbuaji auawe, isipokuwa Yerusalemu. Yerusalemu, Yerusalemu, unawaua wafumbuaji, ukawapiga mawe waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako, kama kuku anavyovikusanya vifaranga vyake mabawani! Lakini hamkutaka! Mtaona, Nyumba yenu ikiachwa, iwe peke yake! Nawaambiani: Hamtaniona tena mpaka siku ile, mtakaposema: Na atukuzwe ajaye kwa Jina la Bwana! *Ikawa, alipoingia siku ya mapumziko nyumbani mwa mkuu wa Mafariseo, ale chakula, wakawa wakimtunduia. Mbele yake mkawamo mtu mwenye ugonjwa wa safura. Yesu akawauliza wajuzi wa Maonyo na Mafariseo akisema: Uko mwiko wa kuponya mtu siku ya mapumziko au hakuna? Wao waliponyamaza, akamshika, akamponya, akamwaga. Kisha akawaambia wale: Kwenu yuko mwenye punda au ng'ombe asiyemwopoa papo hapo, akitumbukia kisimani, hata ikiwa siku ya mapumziko? Nao hawakuweza kumjibu haya. Alipoona, walioalikwa walivyochagua viti vya mbele, akawatolea mfano akiwaambia: Ukialikwa na mtu, uje arusini, usikae penye viti vya mbele! Labda miongoni mwao walioalikwa yumo mwenye ukuu kukupita. Basi, anapokuja mwenye kuwaalika wewe na yeye atakuambia: Mpishe huyu! Ndipo, utakapoanza kupatwa na soni kwa kushika mahali palipo nyuma yao wote. Ila ukialikwa uende, ukakae mahali pa nyuma! Maana mwenye kukualika atakapokuja akuambie: Mwenzangu, sogea mbele huku! Ndipo, utakapotukuzwa mbele yao wote, ambao mnakaa pamoja nao chakulani. Kwani kila anayejikweza mwenyewe atanyenyekezwa, naye anayejinyenyekeza mwenyewe atakwezwa.* Kisha akamwambia yule aliyemwalika: Unapofanya karamu ya mchana au ya jioni usiwaalike rafiki zako wala ndugu zako wala jamaa zako wala majirani walio wenye mali! Maana wasikualike tena, nawe ukapata kulipwa. Ila unapofanya karamu uwaalike wakiwa na wavilema na viwete na vipofu! Ndipo, utakapokuwa mwenye shangwe, kwani hawana cha kukulipa. Maana utalipwa, waongofu watakapofufuka. Mmoja wao walikaa pamoja naye chakulani alipoyasikia haya akamwambia: Mwenye shangwe ndiye atakayekula chakula katika ufalme wa Mungu. *Naye akamwambia: Kulikuwa na mtu aliyetengeneza karamu kubwa, akaalika wengi. Saa ya karamu ilipotimia, akatuma mtumwa wake, aende, awaambie walioalikwa: Njoni! Kwani vyote viko tayari. Wakaanza wote pamoja kuja kujipuzapuza. Wa kwanza akamwambia: Nimenunua shamba, sina budi kwenda, nilitazame; nakuomba, usiniwekee mfundo! Mwingine akasema: Nimenunua ng'ombe kumi wa kuvuta magari, nami ninakwenda, niwajaribu; nakuomba, usiniwekee mfundo! Mwingine akasema: Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja. Basi, mtumwa akarudi, akamsimulia bwana wake. Ndipo, yule mwenye nyumba alipochafuka, akamwambia mtumwa wake: Toka, uende upesi, ufike kwenye viwanja na njia za mjini, ulete wakiwa na wavilema na vipofu na viwete, uwaingize humu! Kisha mtumwa akasema: Bwana, imekwisha fanyika, uliyoniagiza, lakini hamjajaa bado. Naye bwana akamwambia mtumwa: Toka, ufike njiani na nyugoni, uwashurutishe kuingia, nyumba yangu ipate kujaa! Kwani nawaambiani: Waume wale waliokuwa wamealikwa hakuna hata mmoja wao atakayevionja vyakula vyangu.* Walipofuatana naye makundi mengi, akageuka, akawaambia: Mtu akija kwangu asipomchukia baba yake na mama yake na mkewe na watoto wake na ndugu zake wa kiume na wa kike, hata asipoichukia roho yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Naye asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana kwenu yuko mtu anayetaka kujenga mnara, asiyekaa kwanza na kuzihesabu shilingi za jengo, kama anazo za kulitimiza? Kwani akiisha kuweka msingi, asipoweza kumaliza, halafu wote wanaoviona wataanza kumfyoza wakisema: Mtu huyu alianza kujenga, naye hakuweza kumaliza. Au yuko mfalme anayekwenda vitani kushindana na mfalme mwenzake pasipo kukaa kwanza na kufikiri, kama ataweza kuwatuma askari wake elfu kumi, wakutane na yule anayemjia na askari elfu ishirini? Kama haviwezi, atatuma wajumbe, yule mwingine akingali mbali bado, amwombe mapatano. Vivyo hivyo hata kila mmoja wenu asiyeviacha vyote, alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Chumvi ni nzuri, lakini chumvi ikiwa imepotewa na ukolezi itatiwa kiungo gani, ipate kukolea tena? Haitafaa tena, wala kutupwa shambani wala penye mbolea, ile huitupa nje tu. Mwenye masikio yanayosikia na asikie! *Watoza kodi na wakosaji wo wote walipokuwa wanamjia, wamsikilize, Mafariseo na waandishi wakanung'unika wakisema: Huyu huwapokea wakosaji, ale pamoja nao. Ndipo, alipowatolea mfano huu akisema: Kwenu yuko mtu mwenye kondoo mia akipoteza mmoja wao, asiyewaacha wale tisini na tisa porini, aende kumtafuta yule aliyepotea, mpaka atakapomwona? Naye akimwona anamweka mabegani kwa kufurahi. Tena akifika kwao anawaita rafiki zake na majirani zake na kuwaambia: Furahini pamoja nami! Kwani nimemwona kondoo wangu aliyepotea. Nawaambiani: Vivyo hivyo mkosaji mmoja anapojuta, kutakuwako huko mbinguni furaha inayoipita ile iliyoko kwa ajili ya waongofu tisini na tisa wasiopaswa na kujuta. Au yuko mwanamke mwenye shilingi kumi akipoteza moja, asiyewasha taa na kufagia nyumbani na kuitafuta kwa uangalifu, mpaka atakapoiona? Naye akiiona anawaita shoga zake na majirani zake na kusema: Furahini pamoja nami! Kwani nimeiona shilingi yangu, niliyoipoteza. Nawaambieni: Vivyo hivyo mkosaji mmoja anapojuta, itakuwako furaha mbele ya malaika za Mungu.* *Kisha akasema: Kulikuwa na mtu mwenye wana wawili. Aliye mdogo wao akamwambia baba yake: Baba, nipe fungu la mali litakalokuwa langu! Ndipo, alipowagawanyia mali. Siku chache zilipopita, mwana mdogo akavikusanya vyote, akajiendea kufika katika nchi ya mbali. Huko akazitapanya mali zake kwa kuzitumia ovyoovyo tu. Alipoziishia zote pia, njaa kubwa ikaiguia nchi ile, naye akaanza kuumia kwa njaa. Ndipo, alipokwenda kugandamiana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye akamtuma shambani, achunge nguruwe. Akataka sana kulijaza tumbo lake maganda tu, nguruwe waliyokula, lakini hakuna aliyempa. Ndipo, alipojirudia mwenyewe akisema: Vibarua wangapi wako kwa baba yangu wanaoshiba chakula na kusaza, nami hapa ninakufa njaa! Nitainuka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu na wewe; hainipasi tena kuitwa mwana wako, unitumikishe kuwa kama kibarua wako! Kisha akaondoka, akaenda kwa baba yake. Akingali mbali bado, baba yake akamwona, akamwonea uchungu, akapiga mbio, akamkumbatia shingoni, akamnonea. Mwanawe akamwambia: Baba, nimemkosea Mungu na wewe; hainipasi tena kuitwa mwana wako. Lakini baba yake akawaambia watumwa wake: Leteni upesi nguo iliyo nzuri kuliko zote, mmvike! Mtieni hata pete kidoleni na viatu miguuni! Kisha mleteni yule ndama aliyenona, mmchinje, tupate kula na kushangilia! Kwani huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana tena. Wakaanza kushangilia. Lakini mwana wake mkubwa alikuwa shambani; alipokuja na kufika karibu ya mjini akasikia nyimbo na michezo. Akaita mtumwa mmoja, akamwuliza: Mambo hayo ya nini? Naye akamwambia: Ndugu yako amekuja; ndipo, baba yako alipomchinjia yule ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yuko mzima. Akakasirika sana, hakutaka kuingia. Lakini baba yake alipotoka na kumbembeleza, akamjibu baba yake akimwambia: Tazama, miaka hii yote ninakutumikia; tena hakuna agizo lako, nisilolifanya. Nawe hujanipa hata kibuzi, nipate kushangilia na rafiki zangu. Lakini alipokuja huyu mwana wako aliyekula mali zako pamoja na wagoni, umemchinjia yule ndama aliyenona. Naye akamwambia: Mwanangu, wewe siku zote uko pamoja nami, nayo yote, niliyo nayo, ni yako. Lakini imetupasa kushangilia na kufurahi, kwani huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka. Alikuwa amepotea, naye ameonekana tena.* *Akawaambia wanafunzi wake: Kulikuwako mtu mwenye mali aliyekuwa na mtunza mali. Huyu aliposengenywa kwake, ya kuwa anatapanya mali zake, akamwita, akamwambia: Hayo nayasikiaje kwako? Toa hesabu ya utunzaji wako wa mali zangu! Kwani huwezi tena kuzitunza mali zangu. Mtunza mali akasema moyoni mwake: Nifanyeje? Kwani bwana wangu ananiondoa katika utunzaji wa mali. Kulima siwezi; nako kuomba, naona soni. Nimetambua, nitakavyofanya, kusudi wanipokee nyumbani mwao, nitakapoondolewa katika utunzaji wa mali. Akawaita wadeni wa bwana wake kila mmoja, akamwambia wa kwanza: Una deni gani kwa bwana wangu? Aliposema: Matanaki 100 ya mafuta, akamwambia: Kichukue cheti chako, ukae, uandike 50! Kisha akamwambia mwingine: Na wewe una deni gani? Naye aliposema: Makanda 100 ya mchele, akamwambia: Kichukue cheti chako, uandike 80! Naye bwana akamsifu yule mtunza mali mpotovu, ya kuwa alifanya werevu. Kwani wana wa dunia hii huwaendea wa kizazi chao wenye werevu kuliko wana wa mwanga. Nami nawaambiani: Jipatieni rafiki na kutoa mali za nchini zilizo za upotovu, kusudi wawapokee kwenye makao ya kale na kale, mali zitakapokoseka! Aliye mwelekevu wa vitu vilivyo vichache huwa mwelekevu hata wa vile vilivyo vingi. Naye aliye mpotovu wa vitu vilivyo vichache huwa mpotovu hata wa vile vilivyo vingi. Basi, msipokuwa waelekevu wa mali za nchini zilizo za upotovu, yuko nani atakayewapa yaliyo ya kweli?* Nanyi msipokuwa waelekevu wa mali zilizo za wengine, yuko nani atakayewapa zilizo zenu? Hakuna mtumishi anayeweza kutumikia mabwana wawili. Kwani itakuwa hivi: atamchukia wa kwanza na kumpenda wa pili, au atashikamana naye wa kwanza na kumbeza wa pili. Hamwezi kuwatumikia wote wawili, Mungu na Mali za Nchini (Mamona). Mafariseo waliopenda fedha walipoyasikia hayo yote, wakamfyoza. Akawaambia: Ninyi hujipa wongofu wenyewe mbele ya watu, lakini Mungu anaitambua mioyo yenu. Kwani yanayokwezwa na watu huwa chukizo mbele yake Mungu. Mambo ya Maonyo na ya Wafumbuaji yametangazwa mpaka kuja kwake Yohana; toka hapo hutangazwa Utume mwema wa ufalme wa Mungu, tena kila mtu huingizwa kwa nguvu. Kukoma kwao mbingu na nchi ni kwepesi kuliko kupotea kwa kichoro kimoja tu cha Maonyo. Kila mtu anayemwacha mkewe na kuoa mwingine anazini; naye anayeoa mke aliyeachwa na mumewe anazini. *Kulikuwa na mtu mwenye mali aliyevaa nguo za kifalme na za hariri, tena kila siku hula vya urembo vilivyo vizuri sana. Kulikuwako hata maskini, jina lake Lazaro, alikuwa amewekwa mlangoni pake kwa kuwa mwenye vidonda. Akataka sana kushibishwa na makombo yaliyoanguka mezani pake mwenye mali; mbwa nao huja kumlamba vidonda vyake. Ikawa, maskini alipokufa akachukuliwa na malaika, akapelekwa kifuani pa Aburahamu. Kisha mwenye mali akafa naye, akazikwa. Alipokuwa kuzimuni katika maumivu akayainua macho yake, akamwona Aburahamu, yuko mbali, naye Lazaro alikuwa amekaa kifuani pake. Akaita akisema: Baba Aburahamu, nihurumie! Umtume Lazaro, achovye ncha ya kidole chake majini, aje, aupoze ulimi wangu! kwani naumia humu motoni. Aburahamu akasema: Mwanangu, kumbuka, ya kuwa uliyapokea mema yako katika maisha yako! Lakini Lazaro huko alipata maovu tu. Lakini sasa yeye anatulizwa moyo hapa, nawe wewe unaumia. Tena si kwa ajili hii tu, ila kati yetu sisi nanyi pameatuka ufa mkubwa, kusudi wanaotaka kupita toka hapa, wafike kwenu, wasiweze, wala toka huko wasiweze kupapita, wafike kwetu. Ndipo, alipojibu: Nakuomba, baba, umtume, aende nyumbani kwa baba yangu. Kwani ninao ndugu watano; aje, awashuhudie mambo ya hapa, nao wasije hapa penye maumivu. Aburahamu aliposema: Wanao Mose na Wafumbuaji, na wawasikilize wao! akasema: Sivyo, baba Aburahamu, lakini mtu aliyetoka kwa wafu atakapowaendea, ndipo, watakapojuta. Lakini akamwambia: Wasipomsikia Mose na Wafumbuaji hawataonyeka, hata mtu akifufuka katika wafu.* Kisha akawaambia wanafunzi wake: Makwazo hayana budi kuja, lakini anayeyaleta atapatwa na mambo. Akitundikwa shingoni pake jiwe kubwa la kusagia, kisha atumbukizwe baharini, inamfaa kuliko kukwaza mmoja tu aliye mwenzao hawa wadogo. Jiangalieni! Ndugu yako akikukosea, umtishe! Naye akijuta, umwondolee! Ijapo, akukosee mara saba siku moja na kukurudia mara saba na kusema: Nimejuta, sharti umwondolee! Mitume wakamwambia Bwana: Tuongezee nguvu za kumtegemea Mungu! Bwana akasema: Cheo chenu cha kumtegemea Mungu kikiwa kidogo kama kipunje cha mbegu, mtauambia mkuyu huu: Ng'oka hapo, ulipo, ujipande baharini! nao utawatii. Kwenu yuko mwenye mtumwa wa kulima au wa kuchunga atakayemwambia huyo, akirudi toka shamba: Sasa hivi njoo, ukae chakulani? Hatamwambia: Andalia chakula, nitakachokila, ujifunge nguo, unitumikie, mpaka nitakapokwisha kula na kunywa! Kisha nawe ule, unywe? Je? Atamwambia mtumwa asante, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo nanyi matakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa semeni: Sisi tu watumwa wasiofaa, tumefanya tu yaliyotupasa kuyafanya! *Ikawa, alipokwenda Yerusalemu, akashika njia ya kupita katikati ya Samaria na Galilea. Alipoingia kijijini akakutana na waume kumi wenye ukoma waliokuwa wamesimama mbali, wakapaza sauti wakisema: Bwana Yesu, tuhurumie! Alipowaona akawaambia: Nendeni kujionyesha kwa watambikaji! Ikawa, walipokwenda wakatakaswa. Lakini mmoja wao alipoona, ya kuwa amepona, akarudi akimtukuza Mungu kwa sauti kuu. Akamwangukia kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu akisema: Sio kumi waliotakaswa? Wale tisa wako wapi? Hawakuonekana wengine waliorudi, wamtukuze Mungu, pasipo huyu mgeni? Akamwambia: Inuka, uende zako! Kunitegemea kwako kumekuponya.* *Alipoulizwa na Mafariseo: Ufalme wa Mungu unakuja lini? akawajibu akisema: Ufalme wa Mungu unapokuja, watu hawatauona kwa macho, wala hawatasema: Tazama, up hapa! au: Uko huko! Kwani ufalme wa Mungu umo ndani yenu. Kisha akawaambia wanafunzi: Siku zitakuja, mtakapotunukia kuiona siku moja tu ya siku za Mwana wa mtu, msiione. Nanyi watu watakapowaambia: Tazameni huko! Tazameni hapa! msiende huko, wala msiwafuate! Kwani kama umeme unavyomulika mbinguni toka pembe hii mpaka pembe ile na kuviangaza vilivyoko chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa mtu, siku yake itakapofika. Lakini kwanza imempasa kuteswa mengi na kukataliwa nao wa kizazi hiki. Navyo vilivyokuwa siku za Noa, ndivyo vitakavyokuwa hata siku zile za Mwana wa mtu. Walikuwa wakila, hata wakinywa, walikuwa wakioa, hata wakiozwa mpaka siku, Noa alipoingia katika chombo kikubwa, yakaja mafuriko makubwa ya maji, yakawaangamiza wote. Ndivyo, vilivyokuwa hata siku za Loti: walikuwa wakila, hata wakinywa, wakinunua, hata wakiuza, wakipanda, hata wakijenga. Lakini siku, Loti alipotoka Sodomu, ndipo, moto uliochanganyika na mawe ya kiberitiberiti ulipotoka mbinguni kama mvua, ukawaangamiza wote. Vivyo hivyo vitakuwa siku ile, Mwana wa mtu atakapofunuliwa.* Siku ile mtu atakayekuwapo nyumbani juu, vitu vyake vikiwa nyumbani, asiingie kuvichukua! Vivyo hivyo naye atakayekuwako shambani asivirudie vilivyoko nyuma! Mkumbukeni mkewe Loti! Atakayetafuta kuiponya roho yake ataiangamiza; naye atakayeiangamiza ataiponya, iwepo. Nawaambiani: Usiku ule watu wawili watakaolalia kitanda kimoja, mmoja atapokewa, mwenzake ataachwa. Wake wawili watakaokuwa wakisaga pamoja, mmoja atapokewa, mwenzake ataachwa. Wawili watakaokuwako shambani, mmoja atapokewa, mwenzake ataachwa. Walipojibu na kumwuliza: Wapi, Bwana? akawaambia: Penye nyamafu ndipo, nao tai watakapokusanyikia. Akawaambia mfano wa kwamba: Imewapasa kuomba siku zote pasipo kuchoka, akasema: Katika mji fulani mlikuwa na mwamuzi asiyemwogopa Mungu, wala hakumcha mtu ye yote. Tena mle mjini mlikuwa na mwanamke mjane aliyemwendea mara kwa mara na kusema: Niamua na mpingani wangu! Lakini siku nyingi hakutaka; kisha akasema moyoni mwake: Ijapo, nisimwogope Mungu, wala nisimche mtu ye yote, Lakini kwa sababu ananisumbua, nitamwamulia mjane huyo, mwisho asije, akanipiga machoni. Bwana akasema: Sikilizeni, mwamuzi mwenye upotovu anavyosema! Naye Mungu asiwaamulie aliowachagua, wakimlilia mchana na usiku? Au atawakawilia? Nawaambiani: Atawaamulia upesi. Mwasemaje? Mwana wa mtu atakapokuja ataona wanaomtegemea nchini? *Kulikuwa na watu waliojiwazia wenyewe kuwa waongofu, wakawabeza wengine, akawaambia mfano huu: Watu wawili walipanda kwenda Patakatifu kuomba. Wa kwanza alikuwa Fariseo, wa pili mtoza kodi. Fariseo akasimama, akaomba na kusema hivi moyoni mwake: Mungu, nakushukuru, kwa sababu sifanani na watu wengine walio wanyang'anyi, wapotovu, wagoni, wala sifanani na huyu mtoza kodi. Kila juma nafunga siku mbili, tena ninatoa fungu la kumi la vyote, ninavyovipata. Lakini mtoza kodi akasimama mbali, asitake hata kuyainua macho mbinguni, ila akajipiga kifua akisema: Mungu, nionee huruma mimi niliye mkosaji! Nawaambiani: Huyu alishuka kwenda nyumbani kwake mwenye wongofu kuliko yule. Kwani kila anayejikweza mwenyewe atanyenyekezwa; naye anayejinyenyekeza mwenyewe atakwezwa.* Wakamletea hata vitoto, awaguse. Lakini wanafunzi walipowaona waliwatisha. Ndipo, Yesu alipowaita, waje kwake, akisema: Waacheni vitoto, waje kwangu, msiwazuie! Kwani walio hivyo ufalme wa Mungu ni wao. Kweli nawaambiani: Mtu asiyeupokea ufalme wa Mungu kama kitoto hatauingia kamwe. Kulikuwa na mkubwa, akamwuliza akisema: Mfunzi mwema, nifanye nini, niurithi uzima wa kale na kale? Yesu akamwambia: Unaniitaje mwema? Hakuna aliye mwema, asipokuwa Mungu peke yake tu. Maagizo unayajua, ya kwamba: Usizini! Usiue! Usiibe! Usisingizie! Mheshimu baba yako na mama yako! Naye akasema: Hayo yote nimeyashika, tangu nilipokuwa kijana. Yesu alipoyasikia akamwambia: Umesaza kimoja bado: vyote pia, ulivyo navyo, viuze, uvigawie maskini! Hivyo utakuwa na kilimbiko mbinguni. Kisha uje, unifuate! Lakini alipoyasikia haya, akasikitika sana, kwani alikuwa mwenye mali nyingi. Yesu alipomwona hivyo, akasema: Vitazameni vigumu vinavyowazuia waegemeao mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Masumbuko ya ngamia ya kupenya tunduni mwa sindano ni madogo kuliko yake mwenye mali ya kuuingia ufalme wa Mungu. Wao waliosikia wakasema: Ikiwa hivyo, yuko nani awezaye kuokoka? Akasema: Mambo yasiyowezekana kwa watu huwezekana kwa Mungu. Petero akasema: Tazama, sisi tumeviacha vyetu vyote, tukakufuata wewe. Ndipo, alipowaambia: Kweli nawaambiani: Hakuna mtu aliyeacha nyumba au mkewe au ndugu au wazazi au wana kwa ajili ya ufalme wa Mungu, asiporudishiwa na kuongezwa mara nyingi siku hizi za kuwapo nchini; tena siku zile zitakazokuja ataupata nao uzima wa kale na kale. *Akawatwaa wale kumi na wawili, akawaambia: Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu. Huko Mwana wa mtu aliyoandikiwa na wafumbuaji yatatimizwa yote: atatiwa mikononi mwa wamizimu, afyozwe nao pamoja na kutukanwa na kutemewa mate. Tena watampiga viboko, kisha watamwua. Naye siku ya tatu atafufuka. Lakini hao hawakuyasikia haya hata kidogo, neno hili likawa limefichika, wasilijue maana, wasiyatambue yaliyosemwa. Ikawa, alipokaribia Yeriko, palikuwa na kipofu aliyekaa njiani kando akiomba sadaka. Aliposikia, kundi la watu linapita, akauliza: Kuna nini? Wakamsimulia, ya kuwa Yesu wa Nasareti anapita. Ndipo, alipopaza sauti akisema: Yesu, mwana wa Dawidi, nihurumie! Wao waliotangulia walipomkaripia, anyamaze, yeye akakaza sana kupaza sauti: Mwana wa Dawidi, nihurumie! Ndipo, Yesu aliposimama, akaagiza, aletwe kwake. Alipomfikia, akamwuliza: Wataka, nikufanyie nini? Naye akasema: Bwana, nataka, nipate kuona. Yesu akamwambia: Ona! Kunitegemea kwako kumekuponya. Papo hapo akapata kuona, akamfuata akimtukuza Mungu. Nao watu wote walioviona wakamsifu Mungu. *Alipoingia Yeriko akapita kati ya mji. Mle akaona mtu aliyeitwa jina lake Zakeo, alikuwa mkubwa wa watoza kodi, tena mwenye mali. Alitaka kumwona Yesu, alivyo, lakini hakuweza, kwa sababu watu walikuwa wengi, naye alikuwa mfupi kwa umbo lake. Akapiga mbio, aje mbele, akapanda mtamba, apate kumwona, kwani njia yake ilipitia papo hapo. Yesu alipofika hapo akatazama juu, akamwambia: Zakeo, shuka upesi! Kwani leo sharti nikae nyumbani mwako! Ndipo, aliposhuka upesi, akampokea na kufurahi. Lakini walioviona wakamnung'unikia wote wakisema: Ameingia nyumbani mwake mkosaji na kutua humo. Zakeo akainuka, akamwambia Bwana: Tazama, Bwana, nusu yao vyote, nilivyo navyo, nawapa maskini, tena kama nimepunja mtu, namrudishia mara nne. Lakini Yesu akamwambia: Leo nyumbani humu mmeonekana wokovu, kwani mwenyewe naye ni mwana wa Aburahamu. Kwani Mwana wa mtu amejia kutafuta na kuokoa kilichopotea.* *Watu walipoyasikia hayo, akaongeza kusema na kutoa mfano. Kwa sababu alikuwa karibu ya Yerusalemu, watu wakawaza kwamba: Ufalme wa Mungu sharti utokee sasa hivi. Kwa hiyo akasema: Mtu wa kifalme alikwenda kufika katika nchi ya mbali, ajipatie ufalme, kisha arudi. Akawaita watumwa wake kumi, akawapa mia kumi za shilingi, akawaambia: Zichuuzieni, mpaka nitakaporudi! Lakini wenyeji wake walimchukia, wakatuma wajumbe nyuma yake wakisema: Hatumtaki huyu, atutawale sisi. Ikawa, alipokwisha kuupata ule ufalme, akarudi akaagiza, waitwe wale watumwa, aliowapa fedha, waje kwake, apate kujua, kila mtu alivyojipatia kwa kuzichuuzia. Alipokuja wa kwanza, akasema: Bwana, shilingi zako mia zimeleta mia kumi nyingine. Naye akamwambia: Vema, wewe mtumwa mwema, ulikuwa mwelekevu wa machache, utatwaa miji kumi, uitawale! Alipokuja wa pili, akasema: Bwana, shilingi zako mia zimeleta mia tano. Huyu naye akamwambia: Wewe nawe twaa miji mitano, uitawale! Alipokuja mwingine wao akasema: Bwana, tazama hapa shilingi zako mia! Nimekuwa nimeziweka katika mharuma. Kwani nilikuogopa, kwa kuwa wewe u mkorofi, hutwaa usiyoyaweka, huvuna usioyoyapanda. Akamwambia: Kwa maneno yako wewe ninakuumbua, wewe mtumwa mbaya! Ulinijua, ya kuwa mimi ni mkorofi, hutwaa nisiyoyaweka, huvuna nisiyoyapanda? Basi, kwa nini hukumpa mwenye duka fedha zangu? Nami nilipokuja ningalizichukua pamoja na faida? Akawaambia walioko: Zichukueni shilingi zake mia, mmpe yule mwenye mia kumi! Wakamwambia: Bwana, anazo mia kumi! (Akajibu:) Nawaambiani: Kila mwenye mali atapewa; lakini asiye na kitu, atachukuliwa hata kile, alicho nacho. Lakini wale wachukivu wangu wasionitaka, niwatawale, mwalete hapa, mwachinje mbele yangu!* Alipokwisha kuyasema hayo akaendelea kusafiri, akapanda kwenda Yerusalemu. Ikawa, alipokaribia Beti-Fage na Betania penye mlima unaoitwa Wa Michekele, akatuma wanafunzi wawili akisem: Nendeni katika kijiji kinachowaelekea! Mtakapoingia mle mtaona, pamefungwa mwana punda, ambaye mtu hajampanda bado; mfungueni, mmlete! Kama mtu atawauliza: Mbona mnamfungua? semeni hivi: Bwana wetu anamtakia kazi! Wao waliotumwa walipoondoka kwenda wakaviona, kama alivyowaambia. Walipomfungua mwana punda, wenyewe wakawauliza: Kwa sababu gani mnamfungua mwana punda? Nao wakasema: Bwana anamtakia kazi. Kisha wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao upesiupesi juu ya mwana punda, wakampandisha Yesu. Alipokwenda, wakatandika nguo zao njiani. Alipofika kwenye mtelemko wa mlima wa michekele, wingi wote wa wanafunzi ukaanza kushangilia na kumsifu Mungu wakipaza sauti kwa ajili ya matendo yote ya nguvu, waliyoyaona. Wakasema: Na atukuzwe ajaye kuwa mfalme kwa Jina la Bwana! Mbinguni uko utengemano, nao utukufu uko juu mbinguni! Hapo palikuwa na Mafariseo mle kundini mwa watu, wakamwambia: Mfunzi, wakaripie wanafunzi wako! Akajibu akisema: Nawaambiani: Hawa watakaponyamaza, mawe yatapiga makelele. *Alipofika karibu, akautazama ule mji, akaulilia akisema: Ungaliyatambua na wewe siku hii ya leo yanayokupa utengemano! Lakini sasa yamefichika, macho yako yasiyaone! Kwani siku zitakujia, adui zako watakapokujengea boma, likuzinge, wapate kukuhangisha po pote. Nao watakubomolea wewe na watoto wako waliomo mwako, wasiache mwako jiwe, lishikane na jiwe lenziwe, kwa sababu hukuzitambua siku, ulipokaguliwa. Akapaingia Patakatifu, akaanza kuwafukuza wenye kuchuuzia pale, akawaambia: Imeandikwa: Nyumba yangu sharti iwe nyumba ya kuombea, lakini ninyi mmeigeuza kuwa pango la wanyang'anyi. Kisha akawa akifundishia Patakatifu kila siku. Lakini watambikaji wakuu na waandishi na wakubwa wa watu wakatafuta kumwangamiza, wasione njia ya kuyafanya; kwani watu wote pia walishikamana naye na kumsikiliza.* Ikawa siku moja, alipofundisha watu hapo Patakatifu na kuipiga hiyo mbiu njema, wakamwinukia watambikaji wakuu na waandishi na wazee, wakamwambia wakisema: Utuambie: Hayo unayafanya kwa nguvu gani? au ni nani aliyekupa nguvu hii? Akajibu akiwaambia: Hata mimi nitawauliza neno moja, mnijibu: Ubatizo wake Yohana ulitoka mbinguni au kwa watu? Wakafikiri mioyoni mwao kwamba: Tukisema: Ulitoka mbinguni, atatuuliza: Mbona hamkumtegemea? Lakini tukisema: Ulitoka kwa watu, watu wote watatupiga mawe. Kwani walikuwa wametambua kweli kwamba: Yohana ni mfumbuaji. Kwa hiyo wakajibu: Hatujui, ulikotoka. Ndipo, Yesu alipowaambia: Basi, hata mimi siwaambii nguvu inayonifanyisha hayo. Akaanza kuwatolea watu mfano huu: Mtu alipanda mizabibu, akaipangisha wakulima, kisha akaenda katika nchi nyingine kukaa siku nyingi. Siku zilipotimia, akatuma mtumwa kwa wale wakulima, wampe matunda ya mizabibu. Lakini wakulima wakampiga, wakamrudisha mikono mitupu. Akaongeza kutuma mtumwa mwingine. Naye wale wakampiga na kumtukana, wakamrudisha mikono mitupu. Akaongeza kumtuma wa tatu. Naye wale wakamtia vidonda na kumfukuza. Ndipo, mwenye mizabibu aliposema: Nifanyeje? Nitamtuma mwanangu mpendwa, labla huyo watamcha. Lakini wakulima walipomwona wakafikiri na kusemezana wao kwa wao: Huyu ndiye kibwana; na tumwue, urithi wake uwe wetu! Kwa hiyo wakamsukumasukuma mpaka nje ya mizabibu, wakamwua. Basi, mwenye mizabibu atawafanyia nini? Atakuja na kuwangamiza wakulima hao nayo mizabibu atawapa wengine. Wao waliosikia wakasema: Yasiwe hayo! Naye akawatazama, akasema: Basi, maana ya neno lililoandikwa ni nini? Hilo la kwamba: Jiwe, walilolikataa waashi, hilihili limekuwa jiwe la pembeni? Kila atakayeanguka juu ya jiwe lile atapondeka; naye litakayemwangukia, litambana tikitiki. Saa ileile waandishi na watambikaji wakuu wakatafuta kumkamata, lakini waliliogopa lile kundi la watu; kwani walitambua, ya kuwa amewasemea wao wenyewe mfano lhuo. Wakamtunduia, wakatuma wapelelezi, wafanye ujanja wa kuwa kama waongofu, maana wamnase kwa maneno yake, wapate kumpeleka bomani kwenye nguvu ya mtawala nchi. Nao wakamwuliza wakisema: Mfunzi, tumekujua, ya kuwa unasema ya kweli na kuyafundisha, hutazami nyuso za watu, nayo njia ya Mungu unaifundisha, ilivyo kweli. Sisi tuko na ruhusa ya kumtolea Kaisari kodi, au haiko? Kwa kuujua werevu wao mbaya, akawaambia: Nionyesheni shilingi! Ina chapa na maandiko ya nani? Nao wakasema: Yake Kaisari. Ndipo, alipowaambia: Basi, yaliyo yake Kaisari mtoleeni Kaisari, naye Mungu yaliyo yake Mungu! Hivyo hawakuweza kumnasa kwa maneno yake mbele za watu, wakamstaajabu, alivyojibu, wakanyamaza. Kulikuwa na Masadukeo wanaobisha kwamba: Hakuna ufufuko; wakamjia, wakamwuliza wakisema: Mfunzi, Mose alitundikia: Mtu akifiwa na mkubwa wake aliyekuwa na mkewe pasipo kuwa na mwana, nduguye amchukue huyo mke, amzalie mkubwa wake mwana. Kulikuwa na waume saba walio ndugu. Wa kwanza akaoa mke, akafa pasipo kuwa na mwana. Naye wa pili, kisha wa tatu akamchukua yule mwanamke; vivi hivi hata wale saba, hawakuacha wana walipokufa. Mwisho akafa naye mwanamke. Basi, katika ufuko huyo mwanamke atakuwa mke wa yupi wa hao? Kwani wote saba walikuwa naye yule mwanamke. Yesu akawaambia: Wana wa dunia hii huoa, tena huolewa. Lakini wale watakaopewa kuifikia dunia ile na kufufuliwa katika wafu hawataoa, wala hawataolewa. Kwani hawataweza kufa tena, maana watafanana na malaika, watakuwa wana wa Mungu kwa hivyo, walivyofufuka. Lakini kwa ajili ya wafu, kwamba wafufuliwa, hata Mose alivifumbua kidogo hapo kichakani alipomwita Bwana: Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Lakini Mungu siye wa wafu, la wao walio hai; kwani kwake wote huishi. Kulikuwa na waandishi waliojibu wakisema: Mfunzi, umesema vema. Kwani hawakujipa moyo tena kumwuliza neno. Kisha akawaambia: Husemaje, ya kuwa Kristo ni mwana wa Dawidi? Kwani Dawidi mwenyewe asema katika kitabu cha Mashangilio: Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti kuumeni kwangu, mpaka niwaweke adui zako chini miguuni pako! Basi, Dawidi akimwita Bwana, anakuwaje tena mwana wake? Akawaambia wanafunzi, watu wote waliposikia: Jilindeni kwa ajili ya waandishi wanaotaka kutembea wenye kanzu ndefu, tena hupenda kuamkiwa na watu sokoni! Namo nyumbani mwa kuombea hupenda viti vya mbele, hata wakialikwa chakulani hupenda kukaa penye wakuu. Huzila nyumba za wajane, wakijitendekeza, kama wanakaza kuwaombea. Walio hivyo mapatilizo yao yatakuwa kuliko ya wengine. Alipoinua macho akaona, wenye mali walivyotia sadaka zao katika sanduku ya vipaji. Akaona hata mwanamke mjane aliyekuwa mkiwa, alivyotia mle visenti viwili. Ndipo, aliposema: Kweli nawaambiani: Huyu mjane mkiwa ametia mengi kuliko wote. Kwani hao wote walitoa mali katika mali zao nyingi, wakazitia penye sadaka, lakini huyu kwa ukiwa wake amevitoa vyote, alivyokuwa navyo, ndivyo vilivyomlisha. Wengine waliposema, Patakatifu palivyokuwa pamepambwa na mawe mazuri na mapambo mengine, ndipo, aliposema: Je? Mwayatazama haya? Siku zitakuja, ambapo halitaachwa hata jiwe moja juu ya jiwe lenziwe lisiloporomoshwa chini. Wakamwuliza wakisema: Mfunzi, hayo yatakuwapo lini? Tena kielekezo ni nini, hayo yatakapotimia? Naye akasema: Angalieni, msipotezwe! Kwani wengi watakuja kwa Jina langu na kusema: Mimi ndiye, nazo siku zimekwisha kufika. Msiwafuate hao! Nanyi mtakaposikia vita na mainukiano, msitukutike! Kwani hayo sharti yawepo kwanza; lakini mwisho hauji upesi. Ndipo alipowaambia: Watainukiana taifa na taifa, tena wafalme na wenzao wafalme. Mahali penginepengine patakuwa na matetemeko makuu, pengine na kipindupindu, pengine na njaa. Hata vielekezo vikubwa vitatokea mbinguni vya kuogofya. Lakini hayo yote yatakapokuwa hayajatimia bado, watawanyoshea mikono, wawakamate na kuwakimbiza, wawapeleke nyumbani mwa kuombea namo mabomani, wawaweke mbele yao wafalme na mabwana wakubwa kwa ajili ya Jina langu. Hayo yatawapata ninyi, mje kunishuhudia kwao. Jueni, nguvu imo mioyoni mwenu, msianze kuyahangaikia maneno ya kujikania! Kwani mimi nitawapa vinywani maneno yenye werevu wa kweli; nao wabishi wenu wote hawataweza kuyabisha wala kuyakana. Nanyi mtatolewa na wazazi na ndugu na wenzenu wa ukoo na rafiki; wengine wenu watawaua, nanyi mtakuwa mmechukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. Lakini hata unywele mmoja hautawapotelea vichwani, ila kwa kuvumilia mtazikomboa roho zenu. Lakini hapo mtakapoona, mji wa Yerusalemu ukizungukwa na vikosi, ndipo mjue, ya kuwa kuangamizwa kwake kumetimia. Siku zile watakaokuwako Yudea na wakimbilie milimani! Nao watakaokuwamo mle mjini watoke! Nao watakaokuwako shambani wasiuingie tena! Kwani siku hizo zitakuwa za malipizo, yote yaliyoandikwa yapate kutimizwa. Lakini watakaoona vibaya zaidi ndio wenye mimba na wenye kunyonyesha siku zile. Kwani itakuwa kondo kubwa katika nchi, makali yatakapowatokea watu wa kabila hili: wengine wataanguka kwa ukali wa panga, wengine watatekwa na kutawanyishwa kwenye mataifa yote. Namo Yerusalemu mtakanyagwa na wamizimu, mpaka siku za wamizimu zitakapotimizwa. *Kutakuwa na vielekezo vya jua na vya mwezi na vya nyota. Huku nchini watu wa mataifa yote watapotelewa na mioyo wasipojua maana, mawimbi ya bahari yatakapokaza kuvuma na kutukutika. Ndipo, watu watakapozimia kwa woga na kwa kuyangoja mambo yatakayopajia pote, wanapokaa, kwani hata nguvu za mbingu zitatukutishwa. Hapo ndipo, watakapomwona Mwana wa mtu, anavyokuja katika wingi mwenye nguvu na utukufu mwingi. Lakini hayo yatakapoanza kuwapo, myaelekeze macho yenu mbinguni na kuviinua vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu utakuwa uko karibu! Kisha akawaambia mfano: Utazameni mkuyu na miti yote! Mnapoiona, ikichipua, mnatambua wenyewe, ya kuwa siku za vuli zimekwisha kuwa karibu. Vivyo hivyo nanyi mtakapoyaona hayo, yakiwapo, tambueni, ya kuwa ufalme wa Mungu umewafikia karibu! Kweli nawaambiani: Kizazi hiki hakitakoma, mpaka yatakapokuwapo yote. Mbingu na nchi zitakoma, lakini maneno yangu hayatakoma. Lakini jilindeni, ulafi na ulevi na masumbuko ya nchini yasiwalemee mioyoni, siku ile isiwajie, msipoingoja! Kwani kama mtego unavyonasa, itawajia wote po pote, wanapokaa nchini. Kesheni siku zote na kuomba, mpate nguvu za kuyakimbia hayo yote, yatakayokuwapo, msimamishwe mbele ya Mwana wa mtu!* Akawa kila siku akifundisha Patakatifu, lakini usiku hutoka na kulala kwenye mlima unaoitwa Wa Michekele. Nao watu wote walikuwa wakimwendea asubuhi pale Patakatifu, wamsikilize. Ikawa karibu sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, inayoitwa Pasaka. Nao watambikaji wakuu na waandishi wakatafuta, ndivyo wapate kumwangamiza. Maana walikuwa wakiwaogopa watu wa kwao. Satani akamwingia Yuda anayeitwa Iskariota, naye alikuwa mwenzao wale kumi na wawili. Akaenda zake, akasemezana nao watambikaji wakuu na wakubwa wa askari, ndivyo apate kumtia mikononi mwao. Wakafurahi, wakapatana naye fedha za kumpa. Ndipo, alipowaitikia waziwazi, akatafuta njia iliyofaa ya kumtoa, watu wasijue. Ilipofika siku ya kula mikate isiyotiwa chachu, ndiyo siku iliyopasa kuchinja kondoo ya Pasaka, akamtuma Petero na Yohana akisema: Nendeni, mtuandalie kondoo ya Pasaka, tupate kuila! Nao wakamwambia: Unataka, tukuandalie wapi? Akawaambia: Tazameni, mtakapoingia mjini mtakutana na mtu anayechukua mtungi wa maji, mfuateni mpaka nyumbani, atakamoingia! Mwambieni mwenye nyumba: Mfunzi anakuuliza: Kiko wapi chumba cha kukaa, ndimo niile kondoo ya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu? Ndipo, atakapowaonyesha chumba kikubwa kilichotandikwa, humo tuandalieni! Nao wakaenda, wakaona, kama alivyowaambia, wakaiandaa kondoo ya Pasaka. *Saa ilipofika, akaja kukaa chakulani, nao mitume wakakaa pamoja naye. Akawaambia: Nimetunukia sanasana kuila Pasaka hii pamoja nanyi, nikingali sijateswa bado. Kwani nawaambiani: Sitaila tena, mpaka patakapotimia katika ufalme wa Mungu. Kisha akatwaa kinyweo, akashukuru akisema: Mkitwae hiki, mgawiane wenyewe! Kwani nawaambiani: Tangu sasa sitayanywa tena mazao ya mizabibu, mpaka ufalme wa Mungu utakapokuja. Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema: Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyizeni hivyo, mnikumbuke! Vivyo hivyo akakitwaa nacho kinyweo, walipokwisha kula, akisema: Kinyweo hiki ndicho Agano Jipya katika damu yangu inayomwagwa kwa ajili yenu.* Lakini tazameni, mkono wa mwenye kunichongea upo hapa mezani pamoja nami! Mwana wa mtu anakwenda njia yake, kama alivyotakiwa; lakini yule mtu, ambaye atachongewa naye, atapatwa na mambo. Nao wakaanza kuulizana wao kwa wao: Kwetu sisi yuko nani atakayelifanya jambo hilo? Kukawa mabishano kwao ya kwamba: Kati yetu ni nani aliye mkubwa? Naye akawaambia: Wafalme wa mataifa huwatawala, nao wenye nguvu kwao huitwa mabwana wakubwa, lakini ninyi msiwe hivyo! Ila aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo, naye mwenye kuongoza na awe kama mwenye kutumika! Kwani aliye mkubwa ni yupi? Anayekaa chakulani au anayetumika? Si yule anayekaa chakulani? Lakini mimi kati yenu niko kama mwenye kutumika. Nanyi ndinyi mlioandamana nami katika kujaribiwa kwangu. Kwa hiyo mimi nawawekea ninyi ufalme, kama Baba yangu alivyoniwekea mimi, mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu, nanyi mtakaa katika viti vya kifalme, myahukumu hayo mashina kumi na mawili ya Isiraeli. Simoni, Simoni, tazama, Satani amewataka ninyi, awapepete, kama wanavyopepeta ngano! Lakini mimi nimekuombea, kunitegemea kwako kusikome. Nawe hapo, utakapogukia, uwatie ndugu zako nguvu! Naye akamwambia: Bwana, nikiwa pamoja nawe niko tayari kwenda, ijapo iwe kifungoni, hata kufani. Naye akasema: Nakuambia, Petero: Jogoo hatawika leo, usipokwisha kunikana mara tatu kwamba: Simjui. Akawauliza: Nilipowatuma pasipo mfuko na mkoba na viatu, kulikuwako kitu, mlichokikosa? Wakasema: Hakuna hata kimoja. Akawaambia: Lakini sasa mwenye mfuko na autwae, na mkoba vilevile, naye mwenye kuukosa na auze nguo yake, anunue upanga! Kwani nawaambiani: Lile lililoandikwa sharti litimie kwangu mimi la kwamba: Akahesabiwa kuwa mwenzao wapotovu; kwani naliyoandikiwa hutimia. Nao wakasema: Bwana, tazama, hapa ziko panga mbili! Naye akawaambia: Basi. *Kisha akatoka, akaenda mlimani pa michekele, kama alivyozoea, nao wanafunzi wake wakamfuata. Alipofika pale akawaambia: Mwombe, msije kuingia majaribuni! Akaepukana nao na kuja mbali kidogo kama hapo, mtu anapotupa jiwe, akapiga magoti, akaomba akisema: Baba, ukitaka kipitishe kinyweo hiki, nisikinywe! Lakini yasifanyike, niyatakayo mimi, ila yafanyike uyatakayo wewe! Ndipo, malaika alipomtokea toka mbinguni, akamtia nguvu. Kisha akawa akigombana na kifo, kwa hiyo akajihimiza kuomba, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yaliyodondoka chini. Alipoinuka katika kuomba, akawajia wanafunzi, akawakuta, wamelala usingizi kwa sikitiko, akawaambia: Mbona mmelala usingizi? Inukeni, mwombe, msije kuingia majaribuni!* Angali akisema, mara wakaja kundi la watu, mmoja wao wale kumi na wawili, jina lake Yuda, akiwatangulia, akamkaribia Yesu kumnonea. Yesu akamwambia: Yuda, unamchongea Mwana wa mtu kwa kumnonea? Nao waliokuwa pamoja naye walipoyaona yatakayokuwapo, wakasema: Bwana, tuwapige kwa upanga? Mwenzao mmoja akampiga mtumwa wa mtambikaji mkuu, akamkata sikio la kuume. Lakini Yesu akajibu akisema: Waacheni, wamalize! Akamgusa sikio, akamponya. Kisha Yesu akawaambia waliomjia, wale watambikaji wakuu na wakuu wa Patakatifu na wazee: Mmetoka wenye panga na rungu, kama watu wanavyomwendea mnyang'anyi. Kila siku nilikuwa nanyi hapo Patakatifu, lakini hamkunyosha mikono, mnikamate. Lakini hii ndiyo saa yenu, ndipo, giza linaposhikia nguvu. *Walipokwisha kumkamata, wakampeleka, wamwingize nyumbani mwa mtambikaji mkuu. Lakini Petero akafuata mbalimbali. Walipowasha moto katikati ya ua na kukaa pamoja, naye Petero akaja kukaa katikati yao. Kijakazi alipomwona, akikaa penye mwangaza wa moto, akamkazia macho, akasema: Hata huyu alikuwa pamoja naye. Akakana akisema: Simjui, mama. Punde kidogo mwingine akamwona, akasema: Wewe nawe u mwenzao. Lakini Petero akasema: Mwenzangu, siye mimi. Saa moja ilipopita, mwingine akakaza kusema: Kweli hata huyu alikuwa pamoja naye, kwani ni Mgalilea. Lakini Petero akasema: Mwenzangu, sijui, unavyosema. Angali akisema, papo hapo jogoo akawika. Ndipo, Bwana alipomgeukia Petero, amtazame; hapo Petero akalikumbuka lile neno la Bwana, kama alivyomwambia: Jogoo atakapokuwa hajawika leo, utakuwa umenikana mara tatu. Akatoka nje, akalia sana kwa uchungu.* *Wale waume waliomshika Yesu wakamfyoza na kumpiga, wakamfunika uso, wakamwuliza wakisema: Fumbua! Ni nani aliyekupiga? Hata masimango mengine mengi wakasema na kumtukana. Kulipokucha, wakakusanyika wazee wa kwao na watambikaji wakuu na waandishi, wakampeleka barazani kwa wakuu wao wote. Wakasema: Tuambie, kama wewe ndiwe Kristo! Akawaambia: Nikiwaambia, hamtanitegemea; lakini nikiwauliza, hamtanijibu, wala hamtanifungua. Lakini tangu sasa Mwana wa mtu atakuwa amekaa kuumeni kwa nguvu ya Mungu. Ndipo, waliposema wote: Je? Ndiwe mwana wa Mungu? Naye akawaambia: Ninyi mnasema, kwani nimi ndiye. Nao wakasema: Ushuhuda tunautakia nini tena? Kwani wenyewe tumevisikia, anavyosema.* Kisha wakainuka wale watu wengi wote pia, wakampeleka kwa Pilato. Wakaanza kumsuta wakisema: Huyu tulimwona, anavyowapindua watu wa taifa letu na kuwakataza, wasitoe kodi za Kaisari, akisema: Mimi Kristo ni mfalme. Pilato alipomwuliza akisema: Wewe ndiwe mfalme wa Wayuda? akamjibu akisema: Wewe unavyosema, ndivyo. Pilato akawaambia watambikaji wakuu na makundi ya watu kwake huyu mtu sioni neno la kumhukumu. Lakini wale wakakaza sana kusema: Anawatukusa watu akifundisha katika Yudea yote; naye ameanza Galilea, akafika mpaka hapa. Lakini Pilato alipoyasikia haya akauliza, kama ni mtu wa Galilea. Naye alipotambua, ya kuwa alitoka katika ufalme wa Herode, akamtuma kwa Herode, kwani naye alikuwako Yerusalemu siku zile. Herode alipomwona Yesu akafurahi sana; kwani tangu siku nyingi alikuwa akitaka kumwona, kwa sababu aliyasikia mambo yake, akangojea kuona kielekezo kinachofanyizwa naye. Akamwuliza mengi, lakini yeye hakumjibu neno. Lakini watambikaji wakuu na waandishi waliosimama hapo wakajihimiza kumsuta. Herode pamoja na askari wake walipokwisha kumbeza na kumfyoza, akamvika nguo nyeupe imetukayo, akamrudisha kwa Pilato! Siku ile Herode na Pilato walianza kuwa rafiki, maana siku zilizopita walikuwa wanachukiana. Pilato akawaita watambikaji wakuu na wakubwa na watu wa kwao, wakutane, akawaambia: Mmemleta kwangu mtu huyu, kwamba anawapindua watu; tazameni, mimi nimemwulizauliza mbele yenu, nisione kwake mtu huyu, ya kuwa ameyakosa, mnayomsuta. Hata Herode vile vile hakuona, kwani amemrudisha kwetu. Tazameni, hakukosa neno limpasalo kuuawa. Basi, nitampiga, kisha nitamfungua. Maana ilikuwa imempasa kuwafungulia mmoja kwa desturi ya sikukuu. Watu wote pia wakapiga kelele wakisema: Umwondoe huyu, afe, utufungulie Baraba! Naye Baraba alikuwa ametiwa kifungoni kwa ajili ya kondo iliyokuwamo mjini na kwa ajili ya kuua watu. Pilato akasema nao tena, kwani alitaka kumfungua Yesu. Lakini wakabisha wakisema: Mwambe msalabani! Mwambe msalabani! Ndipo, alipowauliza mara ya tatu: Ni kiovu gani, alichokifanya huyu? Sikuona neno kwake la kumhukumu, auawe; basi, nitampiga, kisha nitamfungua. Lakini wale wakamchokesha kwa kupiga makelele sana wakitaka, awambwe msalabani; ndivyo, makelele yao nayo ya watambikaji wakuu yalivyoshinda. Pilato akakata shauri na kuyaitikia, waliyoyataka: akamfungua yule aliyetiwa kifungoni kwa ajili ya kondo na ya kuua watu, ndiye waliyemtaka; lakini Yesu akamtoa, wamfanyizie watakavyo. Walipompeleka wakamshika Simoni wa Kirene aliyepita akitoka shambani, wakamtwika msalaba, amchukulie Yesu na kumfuata. *Wakamfuata watu wengi mno, hata wanawake waliojipigapiga vifua na kumlilia. Yesu akawageukia, akasema: Enyi wanawake wa Yerusalemu, msinililie mimi, ila mjililie wenyewe na watoto wenu! Kwani tazameni, siku zitakuja, watakaposema: Wenye shangwe ndio wagumba na matumbo yasiyozaa na maziwa yasiyonyonyesha! Ndipo, watakapoanza kuiambia milima: Tuangukieni! na kuyaambia machuguu: Tufunikeni! Kwani mti mbichi wakiufanyizia hivyo huo mkavu utakuwaje? Wakapelekwa nao wengine wawili waliofanya maovu, wauawe pamoja naye. Walipofika mahali panapoitwa Fuvu la Kichwa, wakamwamba msalabani pale yeye na wale wafanya maovu, mmoja kuumeni, mmoja kushotoni. Kisha Yesu akasema: Baba, waondolee! Kwani hawajui wafanyayo.* Hata nguo zake wakazipigia kura, wazigawanyiane. Nao watu walikuwa wamesimama wakitazama; lakini wakuu wakamfyoza wakisema: Wengine aliwaokoa, na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo aliyechaguliwa na Mungu! Nao askari wakamfyoza wakimkaribia na kumpelekea siki wakisema: Kama ndiwe mfalme wa Wayuda, jiokoe! Tena juu yake palikuwa pameandikwa Kigriki na Kiroma na Kiebureo: HUYU NDIYE MFALME WA WAYUDA. *Mwenzao mmoja wale wafanya maovu waliotundikwa akambeza: Wewe siwe Kristo? Jiokoe mwenyewe na sisi! Lakini mwenzake akajibu akimkaripia na kusema: Humwogopi Mungu wewe nawe, uliomo katika mapatilizo yaya haya? Na sisi tumehukumiwa kweli, kwani tunalipizwa yaliyoyapasa matendo yetu; lakini huyu hakuna kipotovu, alichokifanya. Kisha akasema: Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako! Yesu akamwambia: Kweli nakuambia: Leo utakuwa pamoja nami katika Paradiso. Ikawa, ilipofika kama saa sita, pakawa na giza katika nchi yote nzima mpaka saa tisa, kwa kuwa jua liliacha kuwaka; ndipo, pazia la Jumbani mwa Mungu lilipopasuka katikati. Yesu akapaza sauti kuu akisema: Baba, roho yangu naiweka mikononi mwako. Alipokwisha kuyasema haya, pumzi ikamtoka.* Lakini bwana askari alipoliona lililokuwapo akamtukuza Mungu akisema: Kweli mtu huyu alikuwa mwongofu. Nayo makundi yote ya watu waliokuwako kuyatazama hayo, walipoyaona yaliyokuwapo wakarudi kwao na kujipiga vifua. Nao wote waliojuana naye walikuwa wamesimama mbali, hata wanawake waliofuatana naye toka Galilea walikuwako wakiyatazama hayo. Ndipo, palipotokea mtu aliyekuwa mkuu, jina lake Yosefu wa Arimatia, ndio mji wa Wayuda. Huyo alikuwa mtu mwema na mwongofu; kwa hiyo hakujitia katika mashauri na matendo yao; naye alikuwa akiungoja ufalme wa Mungu. Huyo akaenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. Akaushusha msalabani, akaufunga kwa sanda, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajazikwa mtu bado ndani yake. Nayo siku ile ilikuwa ya andalio; ndipo, sikukuu ilipoanzia. Lakini wanawake waliokuja pamoja naye toka Galilea wakafuata, wakalitazama kaburi, tena jinsi mwili wake ulivyowekwa. Kisha wakarudi, wakatengeneza viungo na manukato; lakini siku ya mapumziko wakakaa kimya, kama walivyoagizwa. Siku ya kwanza ya juma wakaenda kaburini asubuhi na mapema wakichukua manukato, waliyoyatengeneza. Wakaliona lile jiwe, limekwisha fingirishwa na kutoka kaburini. Walipoingia, hawakuuona mwili wake Bwana Yesu. Ikawa, walipopotelewa na jambo hili, mara wakawatokea watu wawili waliovaa nguo zimulikazo. Kwa kuingiwa na woga, wakaziinamisha nyuso zao chini; ndipo, wale walipowaambia: Aliye hai mnamtafutiaje penye wafu? Hayumo humu, ila amefufuliwa. Kumbukeni, alivyowaambia alipokuwa bado huko Galilea akisema: Mwana wa mtu sharti atiwe mikononi mwa watu wakosaji, awambwe msalabani, kisha afufuke siku ya tatu! Ndipo, walipoyakumbuka hayo maneno yake, wakarudi toka kaburini, wakawasimulia wale kumi na mmoja na wengine wote haya yote. Nao walikuwa Maria Magadalene na Yohana na Maria, mama yake Yakobo, na wengine waliokuwa pamoja nao; hao ndio waliowapasha mitume habari hizi. Lakini wajapoyawazia maneno hayo kuwa upuzi tu, wasiwaitikie, Petero akainuka, akapiga mbio kufika kaburini, akainama, akachungulia, akaiona sanda tu. Kisha akaenda zake na kulistaajabu moyoni mwake lililokuwapo. *Siku ile wenzao wawili walikuwa wakienda, waje kijijini, jina lake Emao; mtu akitoka Yerusalemu, ni mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakiongeana hayo yote yaliyokuwapo. Ikawa, wakiongea na kuulizana, Yesu mwenyewe akawakaribia, akaenda pamoja nao. Lakini macho yao yalikuwa, kama yamefumbwa, wasipate kumtambua. Alipowauliza: Ni maneno gani hayo, mnayoyaongea hapa njiani? wakasimama na kununa. Mmoja wao, jina lake Kleofa, akajibu akimwambia: Wewe u mgeni peke yako Yerusalemu, usiyatambue yaliyokuwamo siku hizi? Akawauliza: Yapi? Ndipo, walipomwambia: Mambo ya Yesu wa Nasareti! Alikuwa mfumbuaji mwenye nguvu ya kutenda na ya kusema mbele ya Mungu na mbele ya watu wote. Huyo watambikaji wakuu na wakubwa wetu wamemtoa, ahukumiwe kuuawa, wakamwamba msalabani. Lakini sisi twalimngojea, ya kuwa ndiye atakayewakomboa Waisiraeli. Yakiisha hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu hapo, yalipokuwapo. Tena wako wanawake wa kwetu waliotushangaza; walikwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake, wakaja, wakasema: Tumetokewa na malaika waliosema: Yeye yu hai. Tena wako wenzetu waliokwenda kaburini, wakavikuta vivyo hivyo, kama wanawake walivyosema, lakini mwenyewe hawakumwona. Ndipo, alipowaambia: Nyie msiotambua mambo, mnayo mioyo inayokawia kuyategemea yote, Wafumbuaji waliyoyasema. Haikumpasa Kristo kuteswa hivyo, apate kuingia katika utukufu wake? Akaanzia kwa Mose na kwa Wafumbuaji wote, akawaeleza, aliyoandikiwa katika Maandiko yote. Walipokikaribia kijiji, walichokiendea, akajitendekeza, kama anataka kwenda mbele. Lakini wakambembeleza sana wakisema: Fikia mwetu! kwani ni jioni, nalo jua limekwisha kuchwa. Basi, akaingia kufikia mwao. Ikawa, alipokaa chakulani pamoja nao, akautwaa mkate, akauombea, akaumega, akawagawia. Ndipo, macho yao yalipofumbuliwa, wakamtambua. Naye papo hapo alikuwa ametoweka machoni pao. Kisha wakaambiana: Mioyo yetu humu ndani haikuwa ikiwaka moto, aliposema nasi njiani na kutueleza maana ya Maandiko? Wakainuka saa ileile, wakarudi Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja nao waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika na kusema: Bwana amefufuka kweli! Amemtokea Simoni! Nao wakawasimulia, waliyoyaona njiani, na jinsi walivyomtambua, alipoumega mkate.* Walipokuwa wakiongea hivyo, mwenyewe akaja kusimama katikati yao, akawaambia: Tengemaneni! Wakastuka kwa kuingiwa na woga, wakawaza, wameona mzimu. Akawaambia: Mbona mnahangaika hivyo? Tena kwa nini mawazo kama hayo yanawaingia mioyoni mwenu? Yatazameni maganja yangu na miguu yangu, mjue: Ni mimi mwenyewe! Nipapaseni, mwone! Kwani mzimu hanayo nyama ya mwili wala mifupa, kama mnavyoniona mimi kuwa nayo. Alipokwisha kuyasema haya akawaonyesha maganja na miguu. Lakini walipokuwa hawajamtegemea bado kwa kufurahiwa na kwa kushangaa, akawauliza: Mnacho cha kula hapa? Ndipo, walipompa kipande cha samaki kilichokaangwa. Akakitwaa, akakila mbele yao. Kisha akawaambia: Haya ndiyo maneno yangu, niliyowaambia nilipokuwapo bado kwenu, ya kwamba: Sharti yatimizwe yote, niliyoandikiwa katika Maonyo ya Mose na katika wafumbuaji na katika Mashangilio. Ndipo, alipowafumbua akili, waelewe na Maandiko. Akawaambia: Kwa hivyo vilivyoandikwa imempasa Kristo kuteswa na kufufuka katika wafu siku ya tatu; kisha wao wa mataifa yote watatangaziwa kwa Jina lake, wajute, wapate kuondolewa makosa; hivi vianzie Yerusalemu! Nanyi m mashahidi wa mambo haya. Mtaniona mimi, nikituma kwenu kiagio cha Baba yangu! Lakini kaeni tu mjini, mpaka mtakapotiwa nguvu itokayo juu! *Kisha akatoka nao, akawapeleka mpaka Betania; hapo akaiinua mikono yake, akawabariki. Ikawa katika kuwabariki, akajitenga kwao akachukuliwa kwenda mbinguni. Ndipo, walipomwangukia kifudifudi, kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. Wakawapo hapo Patakatifu siku zote wakimtukuza Mungu.* Hapo mwanzo palikuwapo Neno; hilo Neno lilikuwapo kwa Mungu, naye Mungu ndiye aliyekuwa Neno. Hilo lilikuwapo hapo mwanzo kwa Mungu. Vyote viliumbwa nalo, pasipo hilo hakuna hata kimoja kilichoumbwa. Mwake hilo ndimo, uzima ulimokuwa, nao uzima ulikuwa mwanga wa watu. Mwanga huu humulika gizani, lakini giza haikuushika. Palitokea mtu aliyetumwa na Mungu, jina lake Yohana. Huyo alijia kushuhudu, aushuhudie mwanga, wote wapate kuutegemea kwa ajili yake. Mwenyewe hakuwa mwanga, alikuja tu, aushuhudie mwanga. Ndio mwanga wa kweli unaomwangaza kila mtu, tena ndio uliokuwa ukija ulimwenguni. Ulikuwamo ulimwenguni, nao ulimwengu uliumbwa nao, lakini ulimwengu haukuutambua. Alipofika mwake, wao waliokuwa wake hawakumpokea. Lakini wo wote waliompokea aliwapa nguvu, wapate kuwa wana wa Mungu, ndio wale waliolitegemea Jina lake. Hao hawakuzaliwa na damu wala na pendo la mwili wa mtu wala na pendo la mwanamume, ila wamezaliwa na Mungu. Neno lilipopata kuwa mtu, akatua kwetu, nasi tukauona utukufu wake, ni utukufu kama wa mwana aliyezaliwa wa pekee na baba yake, kwani alikuwa mwenye magawio na kweli yote.* *Yohana akamshuhudia yeye na kupaza sauti akisema: Huyu ndiye, niliyemsema: Ajaye nyuma yangu alikuwa mbele yangu, kwani ni mtangulizi wangu. Kwani katika mema yake yaliyo mengi sisi sote tumetwaa magawio kwa magawio. Kwani Maonyo tulipewa na Mose, lakini ugawiaji na ukweli umekuja na Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu hapo kale po pote, Mwana wa Mungu aliyezaliwa wa pekee, aliyeambatana na Baba, ndiye aliyetusimulia.* *Huu ndio ushahidi wa Yohana, Wayuda walipotuma kwake toka Yerusalemu watambikaji na Walawi, wamwulize: Wewe ndiwe nani? Akaungama pasipo kukana, akaungama: Mimi siye Kristo. Walipomwuliza: Sasa je? Ndiwe Elia? akasema: Mimi siye. Ndiwe mfumbuaji? akajibu: Hapana. Wakamwambia: Ndiwe nani? tupate kuwajibu waliotutuma; wajisemaje? Akasema: Ndimi sauti ya mtu apigaye mbiu nyikani: Inyosheni njia ya Bwana, kama alivyosema mfumbuaji Yesaya. Nao waliotumwa walikuwa wa Mafariseo. Walipomwuliza wakimwambia: Mbona unabatiza, kama wewe siwe Kristo wala Elia wala mfumbuaji? Yohana akawajibu: Mimi nabatiza katika maji; lakini kati yenu amesimama, msiyemjua ninyi, ndiye anayekuja nyuma yangu, nami sifai kumfungulia ukanda wa kiatu chake. Haya yalikuwapo huko Betania, ng'ambo ya Yordani, Yohana alikokuwa akibatiza.* Kesho yake akamwona Yesu, akija kwake, akasema: Mtazameni mwana kondoo wa Mungu anayeyaondoa makosa ya ulimwengu! Huyu ndiye, niliyemsema mimi: Nyuma yangu anakuja mtu aliyekuwa mbele yangu, kwani ni mtangulizi wangu. Hata mimi sikumjua; ila kusudi afunuliwe Waisiraeli, ndiyo niliyojia na kubatiza katika maji. Kisha Yohana akamshuhudia akisema: Nimemwona Roho, anavyoshuka toka mbinguni kama njiwa na kumkalia. Nami sikumjua, lakini aliyenituma kubatiza katika maji ndiye aliyeniambia: Utakayemwona, Roho akimshukia na kumkalia, huyo ndiye anayebatiza katika Roho takatifu. Nami nimemwona, nikamshuhudia: Huyu ndiye Mwana wa Mungu. *Kesho yake Yohana akasimama tena na wanafunzi wake wawili, akamtazama Yesu, akitembea, akasema: Mtazameni mwana kondoo wa Mungu! Wale wanafunzi wake wawili waliposikia, akisema hivyo, wakamfuata Yesu. Yesu akageuka, akawatazama, wanavyomfuata, akawauliza: Mwatafuta nini? Nao walipomwuliza: Rabi (maana yake ni kwamba: Mfunzi mkuu), unakaa wapi? akawaambia: Njoni, mwone! Basi, wakaja, wakapaona, anapokaa, wakakaa kwake siku ile, ikawa kama saa kumi. Mmoja wao hao wawili walioyasikia maneno ya Yohana na kumfuata Yesu alikuwa Anderea, ndugu ya Simoni Petero. Huyu akaanza kumwona Simoni aliyekuwa ndugu yake mwenyewe, akamwambia: Tumemwona Masiya (maana yake ni Kristo). Alipokwenda naye kwa Yesu, Yesu akamtazama, akasema: Wewe ndiwe Simoni, mwana wa Yohana, wewe utaitwa Kefa (maana yake: Petero - Mwamba).* *Kesho yake Yesu alipotaka kutoka kwenda Galilea akamwona Filipo, akamwambia: Nifuata! Lakini Filipo alikuwa mtu wa Beti-Saida, ni mji wao Anderea na Petero. Filipo akamwona Natanaeli, akamwambia: Tumemwona, ambaye mambo yake aliyaandika Mose katika Maonyo, hata Wafumbuaji, ndiye Yesu, mwana wa Yosefu wa Nasareti. Natanaeli alipomwambia: Je? Kiko chema kinachoweza kutoka Nasareti? Filipo akamwambia: Njoo, uone! Yesu alipomwona Natanaeli, akija kwake, akasema na kumwelekea kwamba: Tazameni! Mwisiraeli wa kweli asiye na udanganyifu! Natanaeli alipomwuliza: Umenitambua tangu lini? Yesu akajibu, akamwambia: Filipo alipokuwa hajakuita bado, ulipokuwa chini ya mkuyu, hapo nimekuona. Ndipo, Natanaeli alipomjibu: Mfunzi mkuu, wewe ndiwe Mwana wa Mungu, wewe ndiwe mfalme wa Isiraeli. Yesu akajibu, akamwambia: Unanitegemea, kwa sababu nimekuambia: Nimekuona chini ya mkuyu; utaona makubwa kuliko hayo. Kisha akamwambia: Kweli kweli nawaambiani: Mtaona, mbingu zitakavyokuwa zimefunuka, nao malaika wa Mungu wanavyopanda, tena wanavyomshukia Mwana wa mtu.* *Siku ya tatu ilikuwa sikukuu ya arusi huko Kana wa Galilea, hata mamake Yesu alikuwako, naye Yesu na wanafunzi wake wakaalikwa arusini. Mvinyo ilipopunguka, mamake Yesu akamwambia: Hawana mvinyo. Yesu akamwambia: Mama, tuko na jambo gani, mimi na wewe? Saa yangu haijaja bado. Ndipo, mama yake alipowaambia watumishi: Lo lote atakalowaambia, lifanyeni! Pale palikuwa na mitungi sita ya mawe iliyokuwa imewekwa kwa desturi ya kunawa kwao Wayuda; kila mmoja ulienea mabuyu mawili au matatu. Yesu akawaambia: Ijazeni mitungi maji! Walipokwisha kuijaza mpaka juu, akawaambia: Sasa tekeni, mmpelekee mwandaliaji! Basi, wakampelekea. Lakini mwandaliaji hakujua, ilikotoka, watumishi tu waliokuwa wameyateka yale maji walijua. Mwandaliaji alipoyaonja yale maji yaliyogeuka kuwa mvinyo akamwita bwana arusi, akamwambia: Kila mtu hutoa kwanza mvinyo nzuri; watu wakiisha kushiba, huileta isiyo nzuri sana; lakini wewe iliyo nzuri umeiweka mpaka sasa. Huo ndio mwanzo wa vielekezo, Yesu alivyovifanya, nao ulifanyika Kana wa Galilea; ndivyo, alivyoufunua utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamtegemea.* Kisha wakashuka kwenda Kapernaumu, yeye na mama yake na ndugu zake na wanafunzi wake, wakakaa huko siku zisizokuwa nyingi. *Pasaka ya Wayuda ilipokuwa karibu, Yesu akapanda kwenda Yerusalemu. Alipoona hapo Patakatifu wenye kuuzia palepale ng'ombe na kondoo na njiwa, hata wavunjaji wa fedha waliokuwapo wamekaa, akaokota kamba, akazisuka kambaa, akawafukuza wote hapo Patakatufu, hata kondoo na ng'ombe, akazimwaga fedha za wavunjaji na kuziangusha meza zao. Wenye kuuza njiwa akawaambia: Yaondoeni haya hapa! Msiigeuze Nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya uchuuzi! Hapo wanafunzi wake wakakumbuka, ya kuwa imeandikwa: Kwa ajili ya Nyumba yako wivu unanila!* Wayuda walipomwuliza wakimwambia: Unatuonyesha kielekezo gani, kwa kuwa unafanya hivyo? Yesu akajibu akiwaambia: Livunjeni Jumba hili la Mungu! Nami nitalijenga tena muda wa siku tatu. Wayuda wakasema: Jumba hili la Mungu lilijengwa kwa miaka 46, nawe utalijenga kwa siku tatu? Lakini yeye alilisema Jumba la Mungu lililo mwili wake. Hapo, alipokwisha kufufuliwa katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka, ya kuwa aliyasema hayo. Wakayategemea Maandiko na neno hilo, Yesu alilolisema. Lakini alipokuwako Yerusalemu siku za sikukuu ya Pasaka, wengi wakaja kulitegemea Jina lake walipoviona vielekezo vyake, alivyovifanya. Lakini Yesu mwenyewe hakuwategemea, kwamba wanamtegemea, kwani yeye aliwatambua wote; kwa hiyo hakutaka kushuhudiwa na mwingine mambo ya mtu, maana aliyatambua mwenyewe yaliyomo moyoni mwa mtu. *Kulikuwa na mtu wa Mafariseo, jina lake Nikodemo, aliyekuwa mkuu wa Wayuda. Huyo akamjia na usiku, akamwambia: Mfunzi mkuu, tunajua, ya kuwa wewe u mfunzi aliyetoka kwa Mungu, kwani hakuna mtu anayeweza kuvifanya vielekezo hivyo, unavyovifanya wewe, Mungu asipokuwa naye. Yesu akajibu, akamwambia: Kweli kweli nakuambia: Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia: Mtu atawezaje kuzaliwa akiisha kuwa mzee? Ataweza kuingia tena tumboni mwa mama yake, apate kuzaliwa? Yesu akajibu: Kweli kweli nakuambia: Mtu asipozaliwa majini na Rohoni, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu; kilichozaliwa na mwili ni mwili, nacho kilichozaliwa na Roho ni roho. Usistaajabu, nikikuambia: Sharti mzaliwe mara ya pili! Upepo huvuma, upendako, nawe huusikia uvumi wake, lakini hujui, uanziako wala ukomeako. Hivyo ndivyo, kila aliyezaliwa Rohoni alivyo. Nikodemo alipojibu na kumwuliza: Haya yawezekanaje kuwapo? Yesu akajibu, akamwambia: Je? Wewe u mfunzi wa Isiraeli, tena haya huyatambui? Kweli kweli nakuambia: Sisi huyasema, tuyajuayo; huyashuhudia, tuliyoyaona, lakini hamwupokei ushuhuda wetu! Msiponitegemea, nikiwaambia mambo ya ulimwenguni, mtanitegemeaje, nikiwaambia mambo ya mbinguni? Tena hakuna aliyepaa mbinguni, asipokuwa Mwana wa mtu aliyeshuka toka mbinguni. Kama Mose alivyokweza nyoka jangwani, vivyo hivyo hata Mwana wa mtu sharti akwezwe, kila amtegemeaye apate uzima wa kale na kale.* *Kwani kwa hivyo, Mungu alivyoupenda ulimwengu, alimtoa Mwana wake wa pekee, kila amtegemeaye asiangamie, ila apate uzima wa kale na kale. Kwani Mungu hakumtuma Mwana wake ulimwenguni, auhukumu ulimwengu, ila ulimwengu upate kuokolewa naye. Amtegemeaye hahukumiwi; asiyemtegemea amekwisha kuhukumiwa, kwani hakulitegemea Jina la Mwana wa Pekee wa Mungu Nayo hukumu ndiyo hii: mwanga ulikuja ulimwenguni, lakini watu waliipenda giza kuliko mwanga, kwa sababu matendo yao yalikuwa mabaya, kwani kila mwenye kutenda maovu huuchukia mwanga, haji mwangani, matendo yake yasipatilizwe; lakini mwenye kuyafanya yaliyo ya kweli huja mwangani, matendo yake yaonekane, ya kuwa yametendeka katika Mungu.* Kisha Yesu na wanafunzi wake wakaenda katika nchi ya Yudea, akashinda kule pamoja nao akibatiza. Lakini Yohana alikuwa akibatizia Enoni karibu ya Salemu, kwani kule kulikuwa na maji mengi, tena ndiko, watu walikomwendea, wakabatizwa naye, maana Yohana alikuwa hajatiwa bado kifungoni. Ikawa, wanafunzi wa Yohana walipobishana na Myuda kwa sababu ya maosho, wakaja kwa Yohana, wakamwambia: Mfunzi mkuu, aliyekuwa pamoja na wewe kule ng'ambo ya Yordani, yule uliyemshuhudia wewe, tazama, huyo anabatiza, watu wote wakimwendea. Yohana akajibu, akasema: Hakuna, mtu awezacho kukitwaa, asichopewa toka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia, ya kuwa nalisema: Mimi siye Kristo ila nimetumwa, nimtangulie yeye. Aliye mwenye mchumba ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama na kumsikiliza hufurahi sana kwa kuisikia sauti yake bwana arusi; basi, hiyo furaha yangu imetimia. Yeye sharti akue, nami sharti nipunguke. Anayekuja toka juu ni mkuu kuliko wote; aliyetoka chini ni wa nchini, husema yaliyo ya nchini; anayekuja toka mbinguni ni mkuu kuliko wote. Aliyoyaona nayo aliyoyasikia, ndiyo, anayoyashuhudia, lakini hakuna anayeupokea ushuhuda wake. Aupokeaye ushuhuda wake huyu anamtambulisha Mungu waziwazi, kuwa ni wa kweli; kwani aliyetumwa na Mungu huyasema maneno yake Mungu, naye Mungu haigawii Roho kwa kuipima. Baba humpenda Mwana, akampa yote mkononi mwake. Amtegemeaye Mwana anao uzima wa kale na kale, lakini asiyemtii Mwana hataona uzima, ila makali ya Mungu humkalia. Ilikuwa hapo, Bwana akitambua, ya kama Mafariseo wamesikia, ya kuwa Yesu anapata wanafunzi wengi, tena ya kuwa anabatiza kumpita Yohana, ijapo Yesu mwenyewe hakubatiza mtu, ni wanafunzi wake tu. Ndipo, alipoondoka Yudea, akaenda kufika tena Galilea, lakini hakuwa na budi kushika njia ya kupita katikati ya Samaria. *Akafika penye mji wa Samaria, jina lake Sikari, ulio karibu ya kiunga, Yakobo alichompa mwanawe Yosefu; hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Kwa hivyo, Yesu alivyokuwa amechoka kwa mwendo, akakaa pale kisimani; ilikuwa kama saa sita. Alipokuja mwanamke Msamaria kuchota maji, Yesu akamwambia: Nipe, ninywe! kwani wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula. Ndipo, yule mwanamke Msamaria alipomwambia: Wewe uliye Myuda waniombaje ya kunywa mimi niliye mwanamke wa Kisamaria? Kwani Wayuda na Wasamaria huziana. Yesu akajibu, akamwambia: Kama ungekijua kipaji cha Mungu, tena kama ungemjua anayekuambia: Nipe, ninywe! wewe ungemwomba, naye angekupa maji yenye uzima. Akamwambia: Bwana, hunacho cha kutekea, nacho kisima ni kirefu, basi, utayapata wapi hayo maji yenye uzima? Je? Wewe u mkubwa kuliko baba yetu Yakobo aliyetupa kisima hiki? Naye alikunywa humu mwenyewe na watoto wake na nyama wake wa kufuga. Yesu akajibu, akamwambia: Kila anayeyanywa maji haya ataona kiu tena; lakini atakayeyanywa maji, nitakayompa mimi, hataona kiu kale na kale. Ila maji yale, nitakayompa, yatakuwa mwilini mwake chemchemi ya maji yabubujikayo, yamfikishe penye uzima wa kale na kale.* Yule mwanamke alipomwambia: Bwana, nipe maji hayo, nisipate kuona kiu tena, wala nisije hapa tena kuchota! akamwambia: Nenda, umwite mumeo! Kisha urudi hapa! Yule mwanamke alipojibu na kusema: Sina mume, Yesu akamwambia: Umesema kweli: Sina mume. Kwani waume watano ulikuwa nao, naye uliye naye sasa, siye mume wako; hili umesema kweli. Ndipo, yule mwanamke alipomwambia: Bwana, nakuona, ya kuwa wewe u mfumbuaji. Baba zetu walitambikia mlimani huku, nanyi husema: Yerusalemu ndipo, panapopasa kupatambikia. *Yesu akamwambia: Nitegemea mama, ya kuwa saa inakuja, itakapokuwa, msimtambikie Baba wala huku mlimani wala Yerusalemu! Ninyi hutambikia, msichokijua; sisi hutambikia, tunachokijua, kwani wokovu umeanzia kwa Wayuda. Lakini saa inakuja, tena sasa iko, wenye kutambika kweli watakapomtambikia Baba kiroho na kikweli, kwani naye Baba huwataka wanaomtambikia hivyo. Mungu ni Roho, nao wanaomtambikia imewapasa kumtambikia kiroho na kikweli.* Ndipo, yule mwanamke alipomwambia: Najua, ya kuwa Masiya anakuja anayeitwa Kristo; yeye atakapokuja atatufunulia yote. Yesu akamwambia: Mimi ndiye ninayesema nawe. Hapo wanafunzi wake wakaja, wakashangaa, ya kuwa anasema na mwanamke; lakini hakuna aliyeuliza: Watafuta nini? au: Wasemaje naye? Lakini yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda mjini, akawaambia watu: Njoni, mtazame mtu aliyeniambia yote, niliyoyafanya, kama yeye siye Kristo! Ndipo, walipotoka mjini, wakamwendea. *Walipokuwa hawajafika, wanafunzi wakamhimiza wakisema: Mfunzi mkuu, ule! Alipowaambia: Mimi ninacho chakula, msichokijua ninyi, wanafunzi wakasemezana: Yuko mtu aliyemletea chakula? Yesu akawaambia: Chakula changu ni kuyafanya, ayatakayo yeye aliyenituma, niimalize kazi yake. Ninyi hamsemi: Iko miezi minne bado, mavuno yatakapokuwapo? Tazameni, nawaambiani: Yainueni macho yenu, myatazame mashamba! Yamekwisha kuwa meupe, yavunwe. Mvunaji hupokea mshahara, akakusanya vyakula, vimfikishe penye uzima wa kale na kale; hivyo mwishoni mpanzi hufurahi pamoja na mvunaji. Kwani hapo lile fumbo ni la kweli: Mwingine hupanda, mwingine huvuna. Mimi naliwatuma, mvune, msiyoyafanyia kazi; wengine wamefanya kazi, ninyi mkaingia kazini mwao. Kisha Wasamaria wengi wa mji ule wakamtegemea kwa ajili ya neno, yule mwanamke alilomshuhudia kwamba: Ameniambia yote, niliyoyafanya. Kwa hiyo Wasamaria walipomjia wakamtaka, akae kwao. Akakaa huko siku mbili. Kisha waliomtegemea kwa ajili ya neno lake mwenyewe wakawa wengi sana, wakamwambia yule mwanamke: Hatumtegemei tena kwa vile, ulivyotuambia, kwani wenyewe tumemsikia, tukamjua: Ni kweli, huyu ndiye mwokozi wa ulimwengu.* Siku mbili zilipopita, akatoka huko kwenda Galilea. Kwani Yesu mwenyewe alishuhudia, ya kuwa mfumbuaji haheshimiwi kwao, mwenyewe alikokulia. Alipofika Galilea, Wagalilea wakampokea, kwani walikuwa wameyaona yote, aliyoyatenda Yerusalemu siku za sikukuu; kwani nao walikuwa wamekwenda kule siku za sikukuu. Akafika tena Kana wa Galilea, alikogeuza maji kuwa mvinyo. *Kulikuwa na mtu wa kifalme aliyeuguliwa na mwana wake huko Kapernaumu. Huyo aliposikia, ya kuwa Yesu ametoka Yudea, akafika Galilea, akaondoka, akamwendea, akambembeleza, ashuke, amponye mwanawe, kwani alitaka kufa. Lakini Yesu akamwambia: Msipoona vielekezo na vioja hamnitegemei. Yule mtu wa kifalme alipomwambia: Bwana, shuka, mtoto wangu asije kufa! Yesu akamwambia: Jiendee, mwana wako yuko mzima! Yule mtu akalitegemea neno, Yesu alilomwambia, akaenda zake. Angali akishuka, watumwa wake wakaja kukutana naye wakisema: Mtoto wako yuko mzima! Akawauliza saa, alipoanzia kuwa hajambo kidogo. Walipomwambia: Jana saa saba joto limemtoka, baba akatambua, ya kuwa ni saa ileile, Yesu alipomwambia: Mwana wako yuko mzima. Ndipo, yeye nao waliokuwamo mwake walipomtegemea wote. Hiki ndicho kielekezo cha pili, Yesu alichokifanya alipotoka Yudea kwenda Galilea.* *Kisha ilipokuwa sikukuu ya Wayuda, naye Yesu akapanda kwenda Yerusalemu. Kule Yerusalemu karibu ya Lango la Kondoo kulikuwako kiziwa kiitwacho Kiebureo Betesida; hapo palikuwa na vibanda vitano. Humo mlikuwa na wagonjwa wengi, kama vipofu na viwete na wenye kupooza; wote walilala mle wakingoja, maji yatukuswe. Kwani mara kwa mara palishuka malaika kiziwani, akayatikisa maji; hapo, maji yalipoisha kutikiswa, aliyeingia wa kwanza akapona ugonjwa wo wote uliomshika. Pale palikuwa na mtu aliyekuwa hawezi miaka 38. Yesu alipomwona huyo, anavyolala, akatambua, ya kuwa imemwishia hapo miaka mingi, akamwambia: Unataka kuwa mzima? Mgonjwa akamjibu: Bwana, sina mtu wa kunitia kiziwani, maji yanapotikiswa. Kila mara mimi ninapokwenda, mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia: Inuka, jitwishe kitanda chako, upate kwenda zako! Papo hapo yule mtu akawa mzima, akajitwisha kitanda chake, akaenda zake. Lakini siku ile ilikuwa ya mapumziko. Kwa hiyo Wayuda walimwambia yule aliyeponywa: Leo ni siku ya mapumziko, huna ruhusa ya kukichukua kitanda. Lakini akawajibu: Yule aliyenipa kuwa mzima ameniambia: Jitwishe kitanda chako, upate kwenda zako! Wakamwuliza: Nani huyo mtu aliyekuambia: Jitwishe, upate kwenda zako? Lakini yule aliyeponywa hakumjua. Kwani Yesu alikuwa amepaepuka, kwa sababu hapo palikuwa na kundi la watu wengi. Kisha Yesu akamwona Patakatifu, akamwambia: Tazama, umepata kuwa mzima! Usikose tena, maana lisikujie jambo lililo baya kuliko lile!* Ndipo, yule mtu alipoondoka, akawaambia Wayuda: Ni Yesu aliyenipa kuwa mzima. Kwa hiyo Wayuda wakamnyatia Yesu, kwa sababu alivifanyia hivyo siku ya mapumziko. Lakini Yesu akawajibu: Baba yangu hufanya kazi mpaka sasa, nami naifanya. Kwa hiyo Wayuda walikaza kutafuta njia ya kumwua, kwani hakuvunja mwiko tu wa siku ya mapumziko, ila Mungu naye alimwita Baba yake akijilinganisha na Mungu. *Yesu akajibu, akawaambia: Kweli kweli nawaambiani: Hakuna, Mwana awezacho kukifanya kwa nguvu yake, asipokuwa amemwona Baba, anavyokifanya. Kwani yule anavyovifanya, hivyo naye Mwana huvifanya vile vile. Kwani Baba anampenda Mwana, akamwonyesha vyote, anavyovifanya. Nayo matendo yaliyo makubwa kuliko haya atamwonyesha, ninyi mpate kushangaa. Kwani Baba, anavyowaamsha wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uzima, anaowataka. Kwani hata kuhukumu Baba hamhukumu mtu, ila hukumu yote amempa Mwana, wote wapate kumheshimu Mwana, kama wanavyomheshimu Baba. Mtu asiyemheshimu Mwana hamheshimu naye Baba aliyemtuma. Kweli kweli nawaambiani: Mtu anayelisikia neno langu na kumtegemea aliyenituma anao uzima wa kale na kale, hafiki penye hukumu, ila ametoka penye kufa na kuingia penye uzima. Kweli kweli nawaambiani: Saa inakuja na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti yake Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watapata kuwa wazima. Kwani kama Baba alivyo Mwenye uzima, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa Mwenye uzima naye. Akampa nao uwezo wa kuhukumu, kwani ndiye Mwana wa mtu. Msilistaajabu hilo la kwamba: Saa inakuja, ndipo, wote waliomo makaburini watakapoisikia sauti yake. Nao walioyafanya mema watatoka na kufufukia uzima, nao walioyafanya maovu watatoka na kufufukia hukumu.* Mimi siwezi kufanya cho chote kwa shauri langu; nahukumu, kama ninavyosikia; nayo hukumu yangu huwa yenye wongofu, kwani siyatafuti, niyatakayo mimi, ila yeye aliyenituma ayatakayo. Mimi ninapojishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu sio wa kweli. Yuko mwingine anayenishuhudia, nami naujua ushuhuda wake, alionishuhudia, ya kuwa ndio wa kweli. Ninyi mlituma kwa Yohana, naye akayashuhudia yaliyo ya kweli. Lakini mimi sitaki, mtu anishuhudie, ila nayasema haya, ninyi mpate kuokoka. Yule alikuwa taa inayowaka na kuangaza; lakini ninyi mlitaka kushangilia kitambo penye mwanga wake. Lakini mimi ninao ushuhuda ulio mkubwa kuliko wa Yohana. Kwani zile kazi, Baba alizonipa, nizimalize, kazi zizo hizo, ninazozifanya, hunishuhudia, ya kuwa Baba amenituma. Naye Baba aliyenituma yeye amenishuhudia. Ninyi hamjaisikia bado sauti yake, wala hamjaiona sura yake, wala Neno lake hamnalo mioyoni mwenu, likae humo. Kwani yule, aliyemtuma, ndiye, ninyi msiyemtegemea. *Chunguzeni katika Maandiko! Kwani ninyi hudhani: Humo ndimo, mtakamopatia uzima wa kale na kale. Nayo ndiyo kweli yanayonishuhudia. Lakini ninyi hamtaki kuja kwangu, mpate uzima. Mimi sitaki kutukuzwa na watu. Lakini nimewatambua ninyi, ya kuwa hamnao upendo wa Mungu mioyoni mwenu. Mimi nimekuja kwa Jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei. Mwingine atakapokuja kwa jina lake mwenyewe, huyo ndiye, mtakayempokea. Mwawezaje kunitegemea ninyi mnaotukuzana? Lakini utukufu utokao kwake Mungu wa pekee hamwutafuti. Msiniwazie ya kwamba: Mimi nitawasuta kwa Baba; yuko msutaji wenu, ndiye Mose, ninyi mliyemngojea. Kwani kama mngemtegemea Mose, basi, mngenitegemea nami, kwani yeye aliandika mambo yangu mimi. Lakini msipoyategemea, aliyoyaandika yeye, mtayategemeaje, ninayoyasema mimi?* *Kisha Yesu akaondoka kwenda ng'ambo ya bahari ya Galilea iitwayo ya Tiberia. Kundi la watu wengi likamfuata, kwani waliviona vielekezo, alivyowafanyia wagonjwa. Yesu akapanda mlimani, akakaa huko pamoja na wanafunzi wake. Lakini Pasaka ilikuwa karibu, ndiyo sikukuu ya Wayuda. Yesu alipoyainua macho yake, akaona kundi la watu wengi wanaomjia, akamwambia Filipo: Tununue wapi mikate, hawa wapate kula? Hivyo alivisema, amjaribu; kwani mwenyewe alijua, alichotaka kukifanya. Filipo akamjibu: Mikate ya shilingi 200 haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Mmoja wao wanafunzi wake Anderea, nduguye Simoni Petero, akamwambia: Hapa yupo mtoto mdogo, anayo mikate mitano ya mofa na visamaki viwili. Lakini hivyo vitawafaa nini watu walio wengi kama hawa? Yesu akasema: Wakalisheni watu! maana mahali pale palikuwa na majani mengi; waliokaa waume tu walikuwa kama 5000. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia waliokaa; vile vile navyo visamaki, kama walivyotaka. Lakini waliposhiba, akawaambia wanafunzi wake: Yakusanyeni makombo yaliyosalia, pasipatikane kinachopotea! Wakayakusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili makombo ya mikate ile mitano ya mofa yaliyowasalia waliokula. Watu walipokiona kielekezo hicho, alichokifanya, wakasema: Kweli huyu ndiye mfumbuaji atakayekuja ulimwenguni. Yesu alipowatambua, ya kuwa wanataka kuja, wamshike kwa nguvu, wamfanye mfalme, akaondoka tena akaja mlimani yeye peke yake tu. Lakini jua lilipokwisha kuchwa, wanafunzi wake wakatelemka kwenda baharini, wakaingia chomboni, wavuke kwenda Kapernaumu ng'ambo ya bahari. Giza ilipokwisha kuingia, Yesu alikuwa hajafika kwao bado. Namo baharini mkainuka mawimbi kwa upepo uliovuma na nguvu. Walipokwisha endelea mwendo wa nusu saa na kupita kidogo, wakamwona Yesu, anavyokwenda juu ya bahari na kukifikia chombo karibu, wakaogopa. Ndipo, alipowaambia: Ni miye, msiogope! Walipotaka kumwingiza chomboni, mara chombo kikawa ufukoni kwenye nchi, walikokwenda. Kesho yake kundi la watu waliosimama ng'ambo ya bahari waliona, ya kuwa hakuwako chombo kingine huko, ni kile kimoja tu. Nao walikuwa wameona, ya kuwa Yesu hakuingia chomboni pamoja na wanafunzi wake; waliona, wanafunzi wake walivyoondoka peke yao. Lakini vyombo vingine vilivyotoka Tiberia vikafika karibu ya mahali pale, walipokula mikate, Bwana akiiombea. *Watu walipoona, ya kuwa Yesu hayuko, ya kuwa wanafunzi wake hawako nao, wakaingia katika vile vyombo, wakafika Kapernaumu, wamtafute Yesu. Walipomwona ng'ambo ya bahari wakamwuliza: Mfunzi mkuu, umefika lini hapa? Yesu akawajibu akisema: Kweli kweli nawaambiani: Hamnitafuti, kwa maana mmeona vielekezo, ila kwa maana mmeila ile mikate, mkashiba. Sumbukieni vyakula! Lakini vile vinavyoangamia sivyo, ni vile vinavyokaa, viwafikishe penye uzima wa kale na kale, navyo ndivyo, Mwana wa mtu atakavyowapani ninyi. Kwani huyu ndiye, Baba Mungu aliyemwagiza hivyo na kumtia muhuri. Walipomwuliza: Tufanyeje, tupate kuzisumbukia kazi za Mungu? Yesu akajibu, akawaambia: Hii ndiyo kazi ya Mungu, mkimtegemea yeye, aliyemtuma.* Wakamwambia tena: Wewe unafanya kielekezo gani, tukione, tukutegemee? Wewe unasumbukia nini? Baba zetu walikula Mana jangwani, kama ilivyoandikwa: Aliwapa mikate iliyotoka mbinguni, waile. Yesu akawaambia: Kweli kweli nawaambiani: Mose siye aliyewapa ninyi mikate iliyotoka mbinguni, ila Baba yangu ndiye anayewapa ninyi mkate wa kweli utokao mbinguni. Kwani mkate wa Mungu ndio ule ushukao toka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Ndipo, walipomwambia: Bwana, tupe siku zote mkate huo! Yesu akawaambia: Mimi ndio mkate wa uzima; ajaye kwangu hataona njaa, naye anitegemeaye hataona kiu hata siku moja. Lakini ndivyo, nilivyowaambia: Mmeniona, lakini hamnitegemei. Wote, Baba anipao, ndio watakaokuja kwangu; naye ajaye kwangu sitamfukuza, ajiendee. Kwani sikushukia toka mbinguni kuyafanya mapenzi yangu mimi, ila mapenzi yake yeye aliyenituma. Nayo mapenzi yake yeye aliyenituma ndiyo haya: wote, alionipa, nisiwapoteze hata mmoja wao, ila niwafufue siku ya mwisho. Kwani haya ndiyo mapenzi ya Baba yangu: kila anayemtazamia Mwana na kumtegemea apate uzima wa kale na kale, nami nitamfufua siku ya mwisho. Wayuda wakamnung'unikia, kwa sababu alisema: Mimi ndio mkate ulioshuka toka mbinguni, wakasema: Huyu siye Yesu, mwana wa Yosefu? Hatumjui baba yake na mama yake? Asemaje sasa: Nimeshuka toka mbinguni? Yesu akajibu, akawaambia: Msinung'unike ninyi kwa ninyi! Hakuna awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta, nami nitamfufua siku ya mwisho. Katika Wafumbuaji yameandikwa ya kwamba: Wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Kila amsikiaye Baba na kujifunza kuja kwangu. Sisemi: Yuko aliyemwona Baba, asipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. *Kweli kweli nawaambiani: Anitegemeaye anao uzima wa kale na kale. Mimi ndio mkate wa uzima. Baba zenu walikula Mana jangwani, kisha wakafa. Huu ndio mkate ushukao toka mbinguni, kwamba: Mwenye kuula asife! Mimi ndio mkate wenye uzima ulioshuka toka mbinguni. Mtu atakayeula mkate huu atakuwa mzima pasipo mwisho. Nao mkate, nitakaowapa mimi, ndio mwili wangu utakaotolewa, ulimwengu upate uzima. Wayuda wakabishana wao kwa wao wakisema: Huyu atawezaje kutupa mwili wake, tuule? Yesu akawaambia: Kweli kweli nawaambiani: Msipoula mwili wa Mwana wa mtu, tena msipoinywa damu yake, hamna uzima mwenu. Mwenye kuula mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa kale na kale, nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwani mwili wangu ni chakula cha kweli, nayo damu yangu ni kinywaji cha kweli. Mwenye kuula mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa mwangu, nami mwake. Kama Baba Mwenye uzima alivyonituma, tena kama mimi nilivyo mzima kwa nguvu ya Baba, vivyo hivyo naye mwenye kunila atakuwa mzima kwa nguvu yangu.* Huo ndio mkate ulioshuka toka mbinguni, si kama ile, baba zenu waliyoila, wakafa. Mwenye kuula mkate huu atakuwa mzima pasipo mwisho. Maneno haya aliyasema akifundisha nyumbani mwa kuombea huko Kapernaumu. *Wengi waliokuwa wanafunzi wake walipoyasikia wakasema: Neno hili ni gumu. Yuko nani awezaye kulisikia? Lakini Yesu kwa kujua moyoni mwake, ya kuwa wanafunzi wake wanalinung'unikia hilo, akawaambia: Hili linawakwaza? Vitakuwaje, mkiona, Mwana wa mtu anavyopaa huko, alikokuwa kwanza? Roho ndiyo inayotupatia uzima, mwili haufai kitu. Maneno, niliyowaambia, ndiyo ya Kiroho yenye uzima. Lakini kwenu wako wasionitegemea. Kwani tangu mwanzo Yesu aliwajua wasiomtegemea, naye atakayemchongea alimjua vilevile. Akasema: Kwa hiyo nimewaambia: Hakuna awezaye kuja kwangu, asipokuwa amepewa na Baba yangu. Tokea hapo wengi waliokuwa wanafunzi wake wakarudi nyuma, wasifuatane tena naye. Yesu alipowauliza wale kumi na wawili: Nanyi mwataka kujiendea? ndipo, Simoni Petero alipomjibu: Bwana, tumwendee nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa kale na kale. Nasi tumekutegemea, tukatambua, ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mungu Mwenye uzima.* Yesu akawajibu: Mimi sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Tena mmoja wenu ni msengenyaji! Hapo alimsema Yuda wa Simoni, yule Iskariota; kwani huyo ndiye aliyemchongea halafu. Naye alikuwa miongoni mwao wale kumi na wawili. Kisha Yesu alitembea huko Galilea, kwani hakutaka kutembea katika nchi ya Yudea, kwa kuwa Wayuda walitaka kumwua. Lakini sikukuu ya Wayuda iitwayo ya Vibanda ilikuwa karibu. Ndugu zake wakamwambia: Ondoka hapa, uende Yudea, wanafunzi wako nao wapate kuyaona matendo yako, unayoyafanya! Kwani hakuna anayefanya kitu na kujifichaficha akitaka kujulikana waziwazi. Ukifanya hivyo watokee walimwengu, wakujue! Kwani hata ndugu zake hawajamtegemea. Kwa hiyo Yesu akawaambia: Siku zangu hazijafika bado; lakini siku zenu ziko siku zote. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini mimi hunichukia, kwani naushuhudia, ya kuwa matendo yake ni mabaya. Ipandieni ninyi sikukuu hii! Mimi siipandii bado sikukuu hii, kwani siku yangu haijatimia. Alipokwisha kuwaambia hivyo, akasalia Galilea. Lakini ndugu zake walipokwisha kuipandia sikukuu, ndipo, naye alipopanda; lakini hakutokea wazi, alikuwa kama mtu anayejifichaficha. Wayuda walimtafuta penye sikukuu, wakasema: Yuko wapi yule? Kukawa na manung'uniko mengi katika makundi ya watu kwa sababu yake. Wengine walisema: Ni mtu mwema; wengine walisema: Sio, ila hupoteza watu tu. Lakini hapana aliyemsemea mbele ya watu, kwa sababu waliwaogopa Wayuda. Lakini siku za katikati za sikukuu Yesu akapanda kupaingia Patakatifu, akafundisha. Wayuda walipostaajabu wakisema: Huyu anajuaje Maandiko, naye hakufundishwa? Yesu akawajibu, akasema: Mafundisho yangu siyo yangu, ni yake yeye aliyenituma. Mtu akitaka kuyafanya mapenzi yake yeye, atayatambua mafundisho haya, kama yametoka kwake yeye Mungu, au kama nayasema maneno yangu. Mwenye kuyasema yake hutafuta, atukuzwe yeye mwenyewe; lakini mwenye kutafuta, aliyemtuma atukuzwe, huyo ni mtu wa kweli, upotovu wo wote haumo moyoni mwake. Siye Mose aliyewapa Maonyo? Tena kwenu hakuna mtu anayeyafanya Maonyo. Mnatafutiani kuniua? Watu wakajibu: Una pepo! Yuko nani anayetaka kukuua? Yesu akajibu, akawaambia: Ni tendo moja tu, nililolifanya, nanyi nyote mkalistaajabu. Kwa sababu hiyo Mose aliwaagiza kutahiri watu; tena siye Mose aliyeviagiza, ila baba zenu. Nanyi humtahiri mtu hata siku ya mapumziko. Mtu akitahiriwa siku ya mapumziko, kwamba Maonyo ya Mose yasivunjwe, mbona mnanikasirikia mimi, kwa sababu nimeponya mwili wote wa mtu siku ya mapumziko? Msiumbue kwa hivyo tu, mnavyoviona, ila umbueni maumbufu yapasayo! Palikuwa na wenyeji wa Yerusalemu waliosema: Si huyu, wanayemtafuta kumwua? Tazameni, anasema waziwazi, wasimjibu neno! Labda nao wakubwa wetu wametambua kweli, ya kuwa huyu ni Kristo? Lakini huyu tunamjua, anakotoka; lakini Kristo atakapokuja, hakuna atakayetambua, atokako. Ndipo, Yesu alipopaza sauti hapo alipofundishia Patakatifu, akasema: Mimi mnanijua, tena mnakujua, nilikotoka. Lakini sikujileta mwenyewe tu, ila yuko mwenye kweli aliyenituma, msiyemjua ninyi. Mimi ninamjua, kwani nimetoka kwake, naye amenituma. Walipojaribu kumkamata, hata mmoja hakumnyoshea mkono, kwani saa yake ilikuwa haijafika. Lakini wengi waliokuwamo kundini mwa watu wakamtegemea, wakasema: Kristo atakapokuja atafanya vielekezo vingi kuliko hivyo, alivyovifanya huyu? Mafariseo waliposikia, watu wakinong'onezana hayo mambo yake, ndipo, watambikaji wakuu na Mafariseo walipotuma watumishi, wamkamate. *Yesu akasema: Nipo pamoja nanyi bado kidogo; kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma. Mtanitafuta, msinione; napo hapo, nitakapokuwapo, ninyi hamwezi kupafika. Ndipo, Wayuda waliposema wao kwa wao: Huyu anataka kwenda wapi, sisi tusimwone? Atawaendea wale waliotawanyika kwa Wagriki, awafundishe Wagriki? Ni neno gani hilo, alilolisema: Mtanitafuta, msinione? Napo hapo, nitakapokuwapo, ninyi hamwezi kupafika? Siku ya mwisho iliyokuwa kubwa katika sikukuu Yesu alikuwa amesimama, akapaza sauti akisema: Mtu akiwa na kiu na aje kwangu, anywe! Mwenye kunitegemea, kama yalivyoandikwa, mwilini mwake yeye mtatoka mito ya maji yenye uzima. Hivyo alisema kwa ajili ya Roho, watakayepewa waliomtegemea; kwani Roho alikuwa hajaonekana bado, kwa sababu Yesu alikuwa hajaupata utukufu wake.* Wengine waliokuwamo kundini mwa watu walipoyasikia maneno hayo wakasema: Huyu ndiye kweli yule mfumbuaji. Wengine wakasema: Huyu ndiye Kristo, wengine wakasema: Je? Kristo atatoka Galilea? Je? Andiko halikusema: Kristo atatoka katika uzao wa Dawidi mle kijijini mwa Beti-Lehemu, alimokaa Dawidi? Basi, watu wakakosana kwa ajili yake. Wenzao wengine walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyemnyoshea mikono. Kisha wale watumishi wakarudi kwa watambikaji wakuu na kwa Mafariseo; nao walipowauliza: Mbona hamkumleta? watumishi wakajibu: Tangu kale mtu hajasema hivyo kama mtu huyo anavyosema. Mafariseo wakawajibu: Nanyi mmepotezwa? Je? Yuko mkubwa au Fariseo anayemtegemea? Ni hili kundi la watu tu wasioyatambua Maonyo, ndio walioapizwa. Ndipo, Nikodemo aliyemjia siku zile usiku, aliyekuwa mmoja wao, alipowaambia: Maonyo yetu huhukumu mtu, asiposikiwa kwanza, yatambulikane aliyoyatenda? Wakajibu, wakamwambia: Je? Nawe u mtu wa Galilea? Tafuta, uone, ya kuwa hakuna mfumbuaji anayetoka huko Galilea! Wakaenda zao kila mmoja nyumbani kwake. Yesu akaenda zake mlimani pa michekele. Asubuhi na mapema alipokuja tena Patakatifu, watu wote wakamwendea, naye akakaa akiwafundisha. Ndipo, waandishi na Mafariseo walipoleta mwanamke aliyefumaniwa katika ugoni, wakamsimamisha katikati. Kisha wakamwambia: Mfunzi, mwanamke huyu amefumaniwa papo hapo, alipofanya ugoni. Lakini Mose alituagiza katika Maonyo kuwaua wanawake walio hivyo kwa kuwapiga mawe; basi, wewe unasemaje? Lakini walisema hivyo kwa kumjaribu, wapate neno la kumsuta. Yesu akainama chini, akaandika mchangani kwa kidole. Lakini walipokaza kumwuliza, akainua macho, akawaambia: Ninyi, asiye na kosa na aanze kumtupia jiwe! Kisha akainama tena akiandika mchangani. Nao walipoyasikia wakatoka mmojammoja, walioanza ndio wazee. Wakaachwa peke yao, yeye na yule mwanamke aliyekuwa hapo kati. Yesu alipoinua macho, akamwambia: Mama, wako wapi wale waliokusuta? Hakuna aliyekupatiliza? Aliposema: Hakuna, Bwana, Yesu akasema: Basi, hata mimi sikupatilizi; nenda zako! Lakini tangu sasa usikose tena! Kisha Yesu akawaambia tena akisema: Mimi ndio mwanga wa ulimwengu; anifuataye mimi hataendelea kwenda gizani, ila atakuwa anao mwanga wa uzima. Mafariseo wakamwambia: Wewe unajishuhudia mwenyewe; huu ushuhuda wako sio wa kweli. Yesu akajibu, akawaambia: Hata nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio wa kweli; kwani ninajua, nilikotoka, tena ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui, nitokako wala niendako. Ninyi mwahukumu kimtu, mimi sihukumu mtu. Lakini ijapo nihukumu mtu, hukumu yangu ni ya kweli kwani siko peke yangu, ila tuko mimi na yule aliyenituma. Hata katika Maonyo yenu imeandikwa: Ushuhuda wa watu wawili ni wa kweli. Mimi ndiye ninayejishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Wakamwambia: Baba yako yuko wapi? Yesu akajibu: Hamnijui mimi, wala hammjui Baba yangu. Kama mngenijua mimi mngemjua naye Baba yangu. Maneno haya aliyasema penye sanduku ya vipaji alipofundishia Patakatifu. Lakini hata mmoja hakumkamata, kwani saa yake ilikuwa haijafika. Akawaambia tena: Mimi nakwenda zangu, nanyi mtanitafuta, hata kufa mtakufa, mko katika ukosaji wenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kukufika. Wayuda wakasema: Je? Atajiua mwenyewe akisema: Niendako mimi, ninyi hamwezi kukufika? Akawaambia: Ninyi mmetoka huku nchini, mimi nimetoka huko juu. Ninyi mmetoka humu ulimwenguni, mimi sikutoka humu ulimwenguni. Kwa hiyo naliwaambia: Kufa mtakufa, mko katika ukosaji wenu. Kwani msiponitegemea, ya kuwa mimi ndiye, mtakufa, mko katika ukosaji wenu. Wakamwambia: Wewe ndiwe nani? Yesu akawaambia: Nimewaambia tangu mwanzo, kwa sababu gani niiseme tena? Kama ningeyasema yale mengi, mliyoyafanya, ningewaumbua; lakini aliyenituma ni wa kweli, nami niliyoyasikia kwake, ndiyo, ninayoyasema ulimwenguni. Hawakutambua, ya kuwa aliwaambia mambo ya Baba. Kisha Yesu akasema: Hapo, mtakapomkweza Mwana wa mtu, ndipo, mtakapotambua, ya kuwa mimi ndiye. Hakuna ninayoyafanya kwa mapenzi yangu, ila Baba aliyonifundisha ndiyo, ninayoyasema. Naye aliyenituma yuko pamoja nami; hakuniacha peke yangu, kwani mimi siku zote nayafanya, yanayompendeza. Alipoyasema haya, wengi wakamtegemea. *Hao Wayuda waliomtegemea Yesu akawaambia: Ninyi mkilikalia Neno langu, kweli m wanafunzi wangu, mwitambue iliyo ya kweli, nayo iliyo ya kweli itawakomboa. Wakamjibu: Sisi tu uzao wake Aburahamu, hatujawa bado watumwa wa mtu, nawe wasemaje: Mtakombolewa? Yesu akawajibu: Kweli kweli nawaambiani: Kila afanyaye makosa ni mtumwa wa makosa. Naye mtumwa hakai nyumbani kale na kale, lakini mwana ndiye akaaye kale na kale. Basi, huyo Mwana atakapowakomboa, mtakuwa mmekombolewa kweli.* Ninajua, ya kuwa ninyi m uzao wake Aburahamu. Lakini mnatafuta kuniua, kwani ndani yenu Neno langu halipati pa kukaa. Mimi niliyoyaona kwa Baba, ndiyo, ninayoyasema. Nanyi yafanyeni, mliyoyasikia kwake Baba! Ndipo, walipojibu na kumwambia: Baba yetu ni Aburahamu. Yesu akawaambia: Mkiwa watoto wake Aburahamu yafanyeni matendo yake Aburahamu! Lakini sasa mnatafuta kuniua; nami nimewaambia iliyo ya kweli, niliyoisikia kwa Mungu; hivyo Aburahamu hakuvifanya. Ninyi huyafanya matendo ya baba yenu. Wakamwambia: Sisi hatukuzaliwa kwa ugoni. Tunaye baba mmoja, ndiye Mungu. Yesu akawaambia: Mungu kama angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi. Kwani mimi nimetoka kwa Mungu, nikaja huku, lakini sikujijia mwenyewe tu, ila yeye alinituma. Mbona hamyatambui ninayoyasema? Ni kwa sababu hamwezi kulisikia Neno langu. Ninyi mmetoka kwa baba yenu, ni yule Msengenyaji; kwa hiyo mnataka kuzifanya tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa mwua watu tangu mwanzo, hakusimama penye kweli, kwani moyoni mwake hamna iliyo ya kweli. Anaposema uwongo anasema yaliyo yake yeye, kwani ni mwongo na baba yake uwongo. Lakini mimi ninaposema iliyo ya kweli, hamnitegemei. *Kwenu yuko nani anayeweza kuniumbua kuwa mwenye kosa lo lote? Nikisema iliyo ya kweli, mbona ninyi hamnitegemei? Aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu. Kwa hiyo ninyi hamyasikii, kwani ninyi ham wa Mungu. Wayuda wakajibu, wakamwambia: Sisi hatusemi kweli: Ndiwe Msamaria? Tena una pepo? Yesu akajibu: Mimi sina pepo, ila ninamheshimu Baba yangu, nanyi mwanibeza. Lakini mimi sitafuti, nitukuzwe. Yuko anayevitafuta na kuhukumu. Kweli kweli nawaambiani: Mtu atakapolishika Neno langu hataona kufa kale na kale. Ndipo, Wayuda walipomwambia: Sasa tumekutambua, ya kuwa una pepo. Aburahamu amekufa, nao wafumbuaji wamekufa, na wewe wasema: Mtu atakapolishika Neno langu hataona kufa kale na kale? Je? Wewe u mkubwa kuliko baba yetu Aburahamu aliyekufa? Nao wafumbuaji wamekufa. Wajifanya kuwa nani? Yesu akajibu: Nikijipa utukufu mwenyewe, utukufu wangu ni wa bure; lakini Baba yangu ndiye anayenipa utukufu, ni yeye, mnayemsema ninyi: Ni Mungu wetu. Nanyi hamkumtambua yeye, lakini mimi nimemjua. Nami kama ningesema: Simjui, ningefanana nanyi kuwa mwongo. Lakini nimemjua, nalo Neno lake ninalishika. Baba yenu Aburahamu alishangilia, kwamba aione siku yangu; akaiona, akafurahi. Wayuda wakamwambia: Hujapata bado miaka 50, nawe umemwona Aburahamu? Yesu akawaambia: Kweli kweli nawaambiani: Aburahamu alipokuwa hajakuwapo bado, mimi nilikuwa nipo. Ndipo, walipookota mawe, wamtupie. Lakini Yesu akawa amefichika, akapatoka patakatifu.* Alipokuwa akitambea akaona amtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wakamwuliza wakisema: Mfunzi mkuu, aliyekosa ni nani? Huyu au wazazi wake, akizaliwa kipofu? Yesu akajibu: Hawakukosa wala huyu wala wazazi wake, ila alizaliwa hivyo, kazi ya Mungu ionekane kwake. Sisi sharti tuzifanye kazi zake aliyenituma, mchana ukingali upo. Usiku unakuja, pasipowezekana kufanya kazi. Nikingali ulimwenguni, mimi ndio mwanga wa ulimwengu. Alipokwisha kuyasema haya akatena mate chini, akayavuruga hayo mate kuwa kitope, nacho kitope akampaka machoni, akamwambia: Nenda, unawe katika ziwa la Siloa, ni kwamba: Aliyetumwa. Basi, akaenda, akanawa, akarudi mwenye kuona. Majirani zake nao waliomwona siku zote, alivyokaa na kuombaomba, wakasema: Huyu siye aliyekuwa amekaa na kuombaomba? Wengine wakasema: Ndiye; wengine wakasema: Siye, wamefanana tu; yeye akasema: Mimi ndiye. Basi, wakamwuliza: Macho yako yamefumbukaje? Akajibu: Yule mtu anayeitwa Yesu alivuruga kitope, akanipaka machoni, akaniambia: Uende penye ziwa la Siloa, unawe! Nikaenda, nikanawa, nikapata kuona. Walipomwuliza: Yuko wapi huyo? akasema: Sijui. Wakampeleka kwa Mafariseo yule aliyekuwa ni kipofu. Lakini siku, Yesu alipokivuruga kitope na kumfumbua macho yake, ilikuwa ya mapumziko. Mafariseo walipomwuliza tena, alivyopata kuona, akawaambia: Alinipaka kitope machoni, nikanawa, ndio naona. Kwao Mafariseo walikuwako waliosema: Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwani haishiki miiko ya siku ya mapumziko. Wengine waliposema: Mtu mkosaji awezaje kuvifanya vielekezo kama hivyo? wakakosana wao kwa wao. Kwa hiyo wakamwambia kipofu tena: Wewe unamwona kuwa nani, kwa sababu alikufumbua macho? Naye akasema: Ni mfumbuaji. Basi, Wayuda hawakulisadiki neno lake, ya kuwa alikuwa ni kipofu, akapata kuona, mpaka walipowaita wazazi wake yeye aliyepata kuona; wakawauliza: Huyu ndiye mwana wenu, mnayemsema: Alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona? Wazazi wake wakajibu, wakasema: Twajua, huyu ni mwana wetu, naye alizaliwa kipofu; lakini hatujui, jinsi alivyopata kuona sasa, wala hatumjui sisi aliyemfumbua macho. Mwulizeni mwenyewe! Ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe. Wazazi wake walisema hivyo kwa kuwaogopa Wayuda, kwani Wayuda walikuwa wamekula njama ya kwamba: Mtu atakayemwungama, kuwa ni Kristo, akatazwe kuiingia nyumba ya kuombea. Kwa hiyo wazazi wake walisema: Ni mtu mzima, mwulizeni mwenyewe! *Kisha wakamwita mara ya pili yule mtu aliyekuwa ni kipofu, wakamwambia: Mtukuze Mungu! Sisi twajua: Mtu huyo ni mkosaji. Yule akajibu: Kama ni mkosaji, sijui; ninalolijua, ni hili moja: Mimi niliyekuwa kipofu naona sasa. Walipomwuliza: Amekufanyia nini? Amekufumbua macho jinsi gani? akawajibu: Nimekwisha kuwaambia; nanyi hamkusikia. Mnatakaje kuvisikia tena? Au nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake? Wakamtukana, wakasema: Wewe ndiwe mwanafunzi wake yule, lakini sisi tu wanafunzi wake Mose. Sisi tunajua, ya kuwa Mungu alisema na Mose, lakini huyo hatumjui, alikotoka. Yule mtu akajibu, akawaambia: Neno hili ni la kustaajabu, ya kuwa ninyi hamjui, alikotoka, naye amenifumbua macho! Twajua, ya kuwa Mungu hasikii wakosaji; ila mtu akimwogopa Mungu na kuyafanya, ayatakayo, basi, huyo humsikia. Tangu hapo kale haijasikiwa, ya kuwa mtu aliyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu. Huyo kama angekuwa hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya kitu. Wakajibu, wakamwambia: Wewe uliyezaliwa wote mzima mwenye makosa, unatufundisha sisi? Wakamfukuza, atoke. Kisha Yesu akasikia, ya kuwa wamemfukuza, atoke; alipomwona akasema: Unamtegemea Mwana wa mtu? Yule akajibu, akasema: Ni yupi, Bwana, nipate kumtegemea? Yesu akamwambia: Umekwisha kumwona, naye anayesema na wewe ndiye. Ndipo, aliposema: Nakutegemea, Bwana! Akamwangukia. Kisha Yesu akasema: Nimekuja katika ulimwengu huu, niuhukumu, wasioona wapate kuona nao waonao wapate kupofuka. Wengine wao Mafariseo waliokuwa pamoja naye walipoyasikia haya wakamwambia: Je? Nasi tu vipofu? Yesu akawaambia: Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa wenye makosa. Lakini sasa mkisema: Twaona, basi, makosa yenu yanawakalia.* Kweli kweli nawaambiani: Asiyepita mlangoni, apate kuingia zizini mwa kondoo, akipandia pengine, huyo ni mwizi na mnyang'anyi. Lakini anayeingia mlangoni ndiye mchungaji wa kondoo. Mlinda mlango anamfungulia huyo, nao kondoo humsikia sauti yake. Naye huwaita kondoo walio wake kwa majina yao, huwatoa nje. Akiisha kuwatoa nje hutangulia mbele yao wote walio wake, nao kondoo humfuata, kwani wameijua sauti yake. Lakini mgeni hawatamfuata, ila watamkimbia, kwani hawazijui sauti za wageni. Fumbo hili Yesu aliwaambia, lakini wale hawakuitambua maana yao, aliyowaambia. Yesu akasema tena: Kweli kweli nawaambiani: Mimi ndio mlango wa kondoo. Wo wote waliokuja mbele yangu ndio wezi na wanyang'anyi; kwa hiyo kondoo hawakuwasikia. Mimi ndio mlango. Mtu akiingilia kwangu mimi ataokoka, atakapoingia napo atakapotoka, apate malisho. Mwizi haji, asipotaka kwiba na kuchinja na kuangamiza. Mimi nimekuja, wakae wenye uzima na wenye vingine vyote. *Mimi ndiye mchungaji mwema; mchungaji mwema hujitoa kwa ajili ya kondoo. Lakini mfanya kazi, asiye mchungaji wala mwenye kondoo, huwaacha kondoo na kukimbia anapomwona chui, akija. Naye chui huwakamata na kuwatawanya. Kwani yeye ni mfanya kazi tu, hawasumbukii kondoo. Mimi ndiye mchungaji mwema, ninawatambua walio wangu, nao walio wangu hunitambua mimi; ndivyo, kama Baba anavyonitambua mimi, na kama mimi ninavyomtambua Baba. Nami mwenyewe ninajitoa, nife kwa ajili ya kondoo. tena ninao kondoo wengine, wasio wa zizi hili; nao hao sharti niwalete, nao wataisikia sauti yangu; kisha watakuwa kundi moja na mchungaji mmoja.* Kwa hiyo Baba ananipenda, kwa sababu najitoa mwenyewe, nife, nipate tena kuwapo. Hakuna anayenishurutisha hivyo, ila mimi ninajitoa mwenyewe. Nina uwezo wa kujitoa, nife, tena nina uwezo wa kuwapo tena. Hivi ndivyo, alivyoniagiza Baba yangu. Wayuda wakakosana tena kwa ajili ya maneno haya. Wengine wao wakasema: Ana pepo, tena yuko na wazimu. Mwamsikilizaje? Wengine wakasema: Maneno haya siyo ya mwenye wazimu. Yuko pepo awezaye kuwafumbua vipofu macho? Kisha pakawa na sikukuu ya mweuo wa Patakatifu huko Yerusalemu; siku zake zilikuwa za kipupwe. *Yesu alipokuwa anatembea hapo Patakatifu katika ukumbi wa Salomo, Wayuda wakamzunguka, wakamwambia: Unatuhangisha roho zetu mpaka lini? Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie waziwazi! Yesu akawajibu: Naliwaambia, nanyi hamnitegemei. Kazi, ninazozifanya katika Jina la Baba yangu, hizo zinanishuhudia. Lakini ninyi hamnitegemei, kwani ninyi hammo katika kondoo wangu. Kondoo wangu huisikia sauti yangu, nami nawajua, nao hunifuata. Nami nawapa uzima wa kale na kale; hawataangamia kale na kale, wala hakuna mtu atakayewapoka mkononi mwangu. Yeye Baba aliyenipa wale ni mkubwa kuliko wote; hakuna mtu anayeweza kuwapoka mkononi mwake Baba. Mimi na Baba tu mmoja.* Wayuda walipookota tena mawe, wamtupie, Yesu akawajibu: Matendo mengi yaliyo mazuri nimewaonyesha kwa nguvu ya Baba; katika hayo ni lipi, mwatakalo kunipigia mawe? Wayuda wakamjibu: Si kwa ajili ya tendo zuri, tukitaka kukupiga mawe, ila kwa ajili ya kumbeza Mungu, kwani wewe uliye mtu unajifanya kuwa Mungu. Yesu akawajibu: Katika Maonyo yenu hamkuandikwa kwamba: Mimi nalisema: Ninyi m miungu? Nalo lililoandikwa haliwezi kutanguliwa. Kama aliwaita wale miungu walioambiwa Neno la Mungu, basi, mimi, ambaye Baba alinitakasa na kunituma ulimwenguni, mwanisemaje: Unambeza Mungu, kwa sababu nalisema: Mimi ni Mwana wake Mungu? Nisipoyafanya matendo ya Baba yangu, msinitegemee! Lakini ninapoyafanya, yategemeeni matendo hayo, msipotaka kunitegemea mimi! Nanyi mpate kujua na kutambua, ya kuwa Baba yumo mwangu, nami nimo mwake Baba. Basi, wakatafuta tena kumkamata, lakini akatoka mikononi mwao. Kisha akaondoka tena kwenda ng'ambo ya Yordani mahali pale, Yohana alipokuwa akibatiza hapo kwanza; akakaa pale. Watu wengi wakamwendea hapo, wakasema: Yohana hakufanya kielekezo cho chote, lakini yote, Yohana aliyoyasema yake huyu, yalikuwa ya kweli. Kwa hiyo wengi wakamtegemea pale. *Kulikuwa na mtu mgonjwa, ndiye Lazaro wa Betania, ni kijiji chao Maria na ndugu yake Marta; Maria ndiye yule aliyempaka Bwana mafuta na kuisugua miguu yake kwa nywele zake. Huyo umbu lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Dada zake wakatuma kwake kwamba: Bwana, tazama, unayempenda ni mgonjwa! Yesu alipovisikia akasema: Ugonjwa huu sio wa kufa, ni wa kuuonyesha utukufu wake Mungu, Mwana wa Mungu apate kutukuzwa nao. Lakini Yesu alikuwa amewapenda akina Marta na ndugu yake na Lazaro. Aliposikia, ya kuwa ni mgonjwa, akakaa siku mbili hapo, alipokuwapo. Kisha ndipo, alipowaambia wanafunzi: Twende Yudea tena! Wanafunzi walipomwambia: Mfunzi mkuu, sasa hivi Wayuda walitafuta kukupiga mawe, nawe unarudi huko tena? Yesu akajibu: Saa za mchana sizo kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai, kwani huuona mwanga wa ulimwengu huu; lakini mtu akienda usiku hujikwaa, kwani mwanga haumo mwake. Alipokwisha kusema hivyo akawaambia: Mpenzi wetu Lazaro amelala, lakini nakwenda, nimwamshe.* Wanafunzi wakamwambia: Bwana, akiwa amelala atapona. Lakini Yesu alikuwa amesema kufa kwake, lakini wale walidhani: alisema kulala usingizi. Ndipo, Yesu alipowaambia waziwazi: Lazaro amekufa. Nami nafurahi kwa ajili yenu, ya kuwa sikuwako kule, mpate kunitegemea. Lakini twende, tufike kwake! Toma anayeitwa Pacha akawaambia wanafunzi wenziwe: Twende nasi, tufe pamoja naye! Yesu alipokuja akamkuta, amekwisha kuwa kaburini siku nne. Lakini kule Betania kulikuwa karibu ya Yerusalemu, ni mwendo wa nusu saa; kwa hiyo Wayuda wengi walikuwa wamekuja kwao Marta na Maria, wawatulize mioyo kwa ajili ya umbu lao. *Marta aliposikia, ya kuwa Yesu anakuja, akaenda kumkuta njiani; lakini Maria alikuwa akikaa nyumbani. Marta akamwambia Yesu: Bwana, kama ungalikuwapo hapa, umbu langu hangalikufa. Lakini na sasa najua, ya kuwa yote, utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu alipomwambia: Umbu lako atafufuka, Marta akamwambia: Najua, ya kuwa atafufuka, wafu watakapofufuka siku ya mwisho. Yesu akamwambia: Mimi ndio ufufuko na uzima; anitegemeaye atapata uzima, ajapokufa. Kila aliye mzima na kunitegemea hatakufa kale na kale. Unavitegemea hivi? Akamwambia: Ndio, Bwana, mimi nimeyategemea, ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, anayekuja ulimwenguni.* Alipokwisha kusema hivyo akaondoka, akamwita ndugu yake Maria na kufichaficha, akasema: Mfunzi yuko, anakwita. Naye alipovisikia akainuka upesi, akamwendea; maana Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado hapo, Marta alipomkuta. Wayuda waliokuwa pamoja naye nyumbani na kumtuliza moyo walipomwona Maria, alivyoinuka upesi na kutoka, wakamfuata wakiwaza, ya kuwa anajiendea kaburini, alie huko. Maria alipofika hapo, Yesu alipokuwa, akamwangukia miguuni alipokwisha kumwona, akamwambia: Bwana, kama ungalikuwapo hapa, umbu langu hangalikufa. Yesu alipoona, anavyolia, nao Wayuda waliokuja pamoja naye wanavyolia nao, akachemka rohoni, akajisisimua, akauliza: Mmemzika wapi? Wakamwambia: Njoo, Bwana, utazame! Naye Yesu machozi yakamtoka. Ndipo, Wayuda waliposema: Tazameni, alivyompenda! Lakini wengine wao wakasema: Huyu aliyemfumbua kipofu macho hakuweza kuzuia, huyu naye asife? Yesu akachemka tena moyoni, akafika penye kaburi; hilo lilikuwa pango lenye jiwe lililowekwa mlangoni pake. Yesu aliposema: Liondoeni hili jiwe! Marta, dada yake aliyekufa, akamwambia: Bwana, ameanza kunuka, kwani leo ni siku ya nne. Yesu akamwambia: Sikukuambia: Ukinitegemea utauona utukufu wake Mungu? Basi, wakaliondoa jiwe. Kisha Yesu akayaelekeza macho juu, akasema: Baba, nakushukuru, ya kuwa umenisikia. Mimi nimekujua, ya kuwa unanisikia po pote; lakini kwa ajili ya kundi la watu wanaosimama hapa ninasema hivyo, wapate kuyategemea, ya kuwa wewe umenituma. Alipokwisha kuyasema haya akaita na kupaza sauti: Lazaro, toka nje! Ndipo, yule aliyekufa alipotoka nje hivyo, alivyokuwa amefungwa kwa sanda miguu na mikono, nao uso wake ulikuwa umefunikwa kwa mharuma. Yesu akawaambia: Mfungueni, mmwache, aende zake! Wayuda wengi waliomjia Maria walipoliona, alilolifanya, wakamtegemea, lakini wengine wao wakaenda zao kwa Mafariseo, wakawaambia, Yesu aliyoyafanya. *Ndipo, watambikaji wakuu na Mafariseo walipoikusanya baraza ya wakuu wote, wakasema: Tufanyeje? Kwani mtu huyu anafanya vielekezo vingi. Tukimwacha hivyo, wote watamtegemea, kisha Waroma watakuja, waichukue nchi yetu pamoja na watu wetu. Lakini mwenzao Kayafa aliyekuwa mtambikaji mkuu wa mwaka ule akawaambia: Ninyi hamjui kitu, wala hamfikiri, ya kuwa inawafalia ninyi, mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kabila lote lisiangamie. Lakini neno hili hakulisema kwa mawazo yake, ila kwa kuwa alikuwa mtambikaji mkuu wa mwaka ule, alifumbua yajayo, kwani Yesu alitumwa afe kwa ajili ya kabila lote; lakini siko kufa kwa ajili ya kabila lake tu, ila ni kwamba, apate kuwakusanya pamoja nao watoto wa Mungu waliotawanyika. Basi, tangu siku ile walikula njama ya kumwua. Naye Yesu hakutembea tena waziwazi kwa Wayuda, ila akaondoka kule, akaenda katika nchi iliyokuwa karibu ya nyikani, akaingia mji uitwao Efuraimu. Mle akakaa pamoja na wanafunzi. Lakini Pasaka ya Wayuda ilikuwa karibu; kwa hiyo wengi wa nchi ile wakapanda kwenda Yerusalemu, Pasaka ilipokuwa bado, wapate kujieua. Kwa kumtafuta Yesu wakasemezana wao kwa wao wakisimama hapo Patakatifu: Mwaonaje? Hatakuja sikukuu hii? Lakini watambikaji wakuu na Mafariseo walikuwa wameagiza, mtu akitambua, alipo, sharti aseme, wapate kumkamata.* Siku sita mbele ya kuwa Pasaka Yesu akaenda Betania, ndiko kwao Lazaro, Yesu aliyemfufua katika wafu. Kule wakamwandalia chakula cha jioni, naye Marta alikuwa akiwatumikia; lakini Lazaro alikuwa mmoja wao waliokaa chakulani naye. Ndipo, Maria alipoleta kichupa cha mafuta ya maua yanayoitwa Narada, ni yenye bei kubwa, nayo yalikuwa hayakuchanganywa na mengine. Akampaka Yesu miguu, kisha akaisugua miguu yake kwa nywele zake; namo nyumbani mote pia mkanukia hayo mafuta ya maua. Yuda Iskariota, mmoja wao wanafunzi wake, ndiye aliyemchongea halafu, akasema: Kwa sababu gani mafuta haya hayakuuzwa kwa shilingi 300, wakapewa maskini? Lakini akisema hivyo, si kwa sababu ya kutunza maskini, ila kwa sababu ya kuwa mwizi; naye ndiye aliyeushika mfuko akivichukua, walivyopewa. Yesu akasema: Umwache! Maana alikuwa ameyawekea siku ya kuzikwa kwangu. Kwani maskini mnao kwenu siku zote, lakini mimi hamwi nami siku zote.* Kundi la Wayuda wengi walipotambua, ya kuwa yuko kule, wakaja, si kwa ajili ya Yesu tu, ila walitaka kumwona naye Lazaro, aliyemfufua katika wafu. Kwa hiyo watambikaji wakuu wakala njama ya kumwua hata Lazaro. Kwani kwa ajili yake yeye Wayuda wengi wakaenda kule, wakamtegemea Yesu. *Kesho yake wale watu wengi walioijia sikukuu waliposikia, ya kuwa Yesu anakuja Yerusalemu, wakachukua makuti ya mitende, wakatoka kumwendea, wakapaza sauti: Hosiana! Na atukuzwe ajaye kwa Jina la Bwana! Ndiye mfalme wa Isiraeli! Yesu alipoona kipunda akampanda, kama ilivyoandikwa: Usiogope, binti Sioni! Tazama, mfalme wako anakuja, amepanda mwana wa punda! Hayo wanafunzi wake kwanza hawakuyatambua, ila Yesu alipokwisha kuupata utukufu wake, ndipo, walipokumbuka, ya kuwa aliandikiwa hayo, tena ndiyo, waliyomfanyizia. Hata wale watu wengi waliokuwa pamoja naye, alipomfufua Lazaro katika wafu na kumwita, atoke kaburini, wakavishuhudia. Kwa sababu hiyo watu wengi wakamwendea, kwani walikuwa wamesikia, ya kuwa yeye amekifanya kielekezo hicho.* Mafariseo wakasemezana wao kwa wao: Tazameni, hakuna mnayoyaweza! Tazameni, watu wote pia wamekwenda kumfuata! *Miongoni mwao waliopanda kutambika siku za ile sikukuu mlikuwa na Wagriki. Hao wakamjia Filipo wa Beti-Saida wa Galilea, wakambembeleza wakisema: Bwana, twataka kumwona Yesu. Filipo akaenda, akamwambia Anderea. Anderea na Filipo wakaenda, wakamwambia Yesu. Ndipo, Yesu alipowajibu akisema: Saa imefika, Mwana wa mtu atukuzwe. Kweli kweli nawaambia: Punje ya ngano isipoanguka mchangani kufia mle, hukaa peke yake yenyewe tu; lakini inapokufa huleta mbegu nyingi. Mwenye kuipenda roho yake huiangamiza; naye mwenye kuichukia roho yake humu ulimwenguni ataiponya, aifikishe penye uzima wa kale na kale. Mtu akinitumikia, sharti anifuate mimi; napo hapo, nilipo mimi, papo hapo hata mtumishi wangu sharti awepo. Mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.* Sasa roho yangu imezizimka, nami nisemeje? Niseme: Baba, uniokoe, nisiifikie saa hiyo? Lakini kwa sababu hiyo nimeijia saa hiyo. Basi, niseme: Baba, ulitukuze Jina lako! Kisha sauti ikaja toka mbinguni kwamba: Nimelitukuza, kisha nitalitukuza tena. Kundi la watu waliokuwako walipoyasikia wakasema: Kumepiga ngurumo; wengine wakasema: Malaika amesema naye. Yesu akajibu akisema: Sauti hii haikutoka kwa ajili yangu, ila kwa ajili yenu. Sasa hukumu ya ulimwengu imetimia; hivi sasa mtawala ulimwengu huu atasukumwa, autoke. Mimi nitakapokwezwa, nitoke nchini, ndipo, nitakapowavuta wote, waje kwangu. Neno hili alilisema, aonyeshe, kama ni kufa gani kulikomngoja. Watu wakamjibu: Sisi tumesikia katika Maonyo: Kristo atakaa kale na kale; tena inakuwaje, wewe ukisema: Mwana wa mtu sharti akwezwe juu? Huyo Mwana wa mtu ni nani? Yesu akawaambia: Mwanga ungaliko kwenu siku chache. Fanyeni mwendo mnapokuwa mnao mwanga, giza isiwaguie! Anayejiendea gizani hajui, anakokwenda. Mkiwa mnao mwanga utegemeeni mwanga, mpate kuwa wana wa mwanga! Yesu alipokwisha kuyasema haya, akaenda zake, akajificha, wasimwone tena. Lakini ijapokuwa amefanya mbele yao vielekezo vingi kama hivyo, hawakumtegemea. Imekuwa hivyo, neno, mfumbuaji Yesaya alilolisema, lipate kutimia: Bwana, yuko nani anayeutegemea utume wetu? Tena yuko nani aliyefumbuliwa, mkono wa Bwana unayoyafanya? Kwa sababu hii hawakuweza kumtegemea, kwani Yesaya alisema tena: Amewapofua macho, akaishupaza mioyo yao, wasije wakaona kwa macho yao, au wakajua maana kwa mioyo yao, au wakageuka, nami nikawaponya. Yesaya aliyasema hayo, kwani aliuona utukufu wake, akayasema mambo yake yeye. Vivyo hivyo hata katika wakubwa walikuwamo wengi waliomtegemea, lakini kwa ajili ya Mafariseo hawakuungama, wasikatazwe kuiingia nyumba ya kuombea. Kwani kutukuzwa na watu walikupenda kuliko kutukuzwa na Mungu. Lakini Yesu alipaza sauti, akasema: Anayenitegemea hanitegemei mimi, ila humtegemea yule aliyenituma. Tena, anayeniona mimi humwona yule aliyenituma. Mimi nimekuja ulimwenguni kuwa mwanga, kila anitegemeaye asikae gizani. Mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu. Kwani sikujia kuuhukumu ulimwengu, ila nimejia kuuokoa ulimwengu. Anikataaye, asiyapokee maneno yangu, anaye atakayemhukumu. Neno, nililolisema, ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho. Kwani mimi sikuyasema maneno yangu, ila Baba mwenyewe aliyenituma ameniagiza, nitakayoyasema na kuyafundisha. Nami nayajua, aliyoyaagiza, ya kuwa ni uzima wa kale na kale. Basi, ninayoyasema, ninayasema, kama Baba alivyoniambia. *Sikukuu ya Pasaka ilipokuwa haijatimia, Yesu alikuwa amejua, ya kuwa saa yake imefika, autoke ulimwengu huu, aende kwa Baba; kwa kuwa aliwapenda watu wake waliomo ulimwenguni, akawapenda mpaka mwisho. Walipokula chakula cha jioni, Msengenyaji alikuwa amekwisha kutia moyoni mwa Yuda wa Simoni Iskariota mawazo ya kumchongea. Kwa hivyo, Yesu alivyojua, ya kuwa Baba alimpa yote mikononi mwake, ya kuwa alitoka kwa Mungu, tena anarudi kwa Mungu, akainuka penye chakula, akaivua kanzu yake, akatwaa kitambaa cha ukonge, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi miguu na kuisugua kwa kile kitambaa, alichojifunga kiunoni. Alipomfikia Simoni Petero, akamwambia; Bwana, wewe unioshe miguu? Yesu akajibu, akamwambia: Ninachokifanya mimi, wewe hukijui sasa, lakini utakitambua halafu. Petero alipomwambia: Hutaniosha miguu kale na kale, Yesu akamjibu: Nisipokuosha, hakuna fungu lako tena lililoko kwangu. Ndipo, Simoni Petero alipomwambia: Bwana, usinioshe miguu tu, nioshe hata mikono na kichwa! Yesu akamwambia: Aliyekwisha koga harudi tena kunawa, isipokuwa miguu, kwani ametakata wote. Nanyi mmetakata, lakini sio wote. Kwani alimjua mwenye kumchongea; kwa hiyo alisema: Hamtakati nyote. Alipokwisha kuwaosha miguu akayatwaa mavazi yake, akakaa tena chakulani, akawaambia; Mwakitambua, nilichowafanyia? Ninyi mnaniita Mfunzi na Bwana, mnasema vema hivyo, kwani ndimi. Basi, mimi niliye Bwana na Mfunzi wenu nikiwaosha ninyi miguu, imewapasa nanyi kuoshana miguu. Kwani nimewapani la kujifunziamo, mfanyiane ninyi kwa ninyi, kama nilivyowafanyia mimi.* Kweli kweli nawaambiani: Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake, wala mjumbe si mkubwa kuliko yule aliyemtuma. Mkiyajua haya m wenye shangwe mkiyafanya. Siyasemi ya ninyi nyote; mimi nawajua, niliowachagua. Lakini sharti andiko litimizwe la kwamba: Anayeula mkate wangu hunipiga mateke. Nawaambia haya sasa, yanapokuwa hayajafanyika bado, kusudi hapo, yatakapofanyika, mpate kuyategemea, ya kuwa mimi ndiye. Kweli kweli nawaambiani: Atakayempokea ye yote, nitakayemtuma, hunipokea mimi; naye mwenye kunipokea mimi humpokea aliyenituma. Yesu alipokwisha kuyasema haya akazizimka jrohoni, akawashuhudia akisema: Kweli kweli nawaambiani: Mwenzenu mmoja atanichongea. Wanafunzi wakatazamana, maana hawakumjua, aliyemsema. Palikuwapo mwanafunzi wake mmoja aliyeegamia kifuani pa Yesu, ndiye, Yesu aliyempenda. Simoni Petero akamkonyeza huyo, amwulize, kama ni nani, anayemsema. Kisha yule aliyemwegamia Yesu kifuani akamwuliza: Bwana, ni nani? Yesu akajibu: Ni yule, mimi nitakayemtowelea kitonge na kumpa. Basi, akatowelea kitonge, akakitwaa, akampa Yuda wa Simoni Iskariota. Alipokwisha kukila kile kitonge, ndipo, Satani alipomwingia. Yesu akamwambia: Utakachokifanya, kifanye upesi! Lakini wale waliokaa chakulani hakuna aliyeitambua sababu ya kumwambia hivyo; wengine wakawaza: kwa sababu Yuda aliushika mfuko wa senti, Yesu alimwambia: Nunua chakula cha siku za sikukuu! au agawie maskini kidogo. Basi, yeye alipokwisha kukipokea kile kitonge akatoka nje papo hapo, lakini ulikuwa usiku. *Yule alipokwisha toka, Yesu akasema: Sasa Mwana wa mtu ametukuzwa, naye Mungu ndiye aliyetukuzwa kwake. Kama Mungu alitukuzwa kwake, yeye Mungu atamtukuza kwake mwenyewe, tena atamtukuza upesi. Vitoto, nipo pamoja nanyi bado kidogo; kisha mtanitafuta, lakini kama nilivyowaambia Wayuda: Ninyi hamwezi kupafika pale, ninapokwenda mimi, ndivyo, ninavyowaambia hata ninyi sasa. Nawapa agizo jipya: Mpendane! Kama nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo! Kwa hiyo wote watatambua, ya kama m wanafunzi wangu mimi, mtakapopendana ninyi kwa ninyi.* Simoni Petero akamwambia: Bwana, unakwenda wapi? Yesu akajibu: Pale ninapokwenda, huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata halafu. Petero akamwambia: Bwana, kwa nini siwezi sasa kufuatana na wewe? Hata roho yangu nitaitoa kwa ajili yako wewe. Yesu akajibu: Uitoe roho yako kwa ajili yangu mimi? Kweli kweli nakuambia: Jogoo hatawika, usipokuwa umekwisha kunikana mara tatu. Mioyo yenu isizizimke! Mtegemeeni Mungu, nami mnitegemee! Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi. Kama visingekuwa hivyo, ningewaambia: Nakwenda kuwatengenezea mahali. Nami ijapokuwa ninakwenda kuwatengenezea mahali, nitakuja tena, niwachukue kuwapeleka mwangu, kwamba nanyi mwepo hapo, nilipo mimi. Nayo njia ya kwenda pale, nitakapokwenda mimi, mmeijua. Ndipo, Toma alipomwambia: Bwana, tusipopajua, unapokwenda, njia tutaijuaje? Yesu akamwambia: Mimi ndiyo njia na kweli na uzima; hakuna atakayefika kwa Baba asiponishika mimi.* Kama mngenitambua mimi, mngemjua hata Baba yangu. Tangu sasa mwamtambua, tena mmemwona. Filipo akamwambia: Bwana, tuonyeshe Baba! hivi vitatutosha. Yesu akamwambia: Miaka hii yote nipo pamoja nanyi, nawe hujanitambua, Filipo? Aliyeniona mimi amekwisha kumwona Baba. Unasemaje: Tuonyeshe Baba? Huyategemei, ya kuwa mimi nimo mwa Baba, naye Baba yumo mwangu mimi? Maneno, ninayowaambia, siyasemi kwa mawazo yangu mwenyewe, ila Baba anayekaa mwangu ndiye anayezitenda kazi zake. Nitegemeeni, ya kuwa mimi nimo mwake Baba, naye Baba yumo mwangu mimi! Lakini mkishindwa, nitegemeeni kwa ajili ya kazi zizo hizo! Kweli kweli nawaambiani: Mwenye kunitegemea naye yeye atazifanya kazi, ninazozifanya mimi, naye atafanya zilizo kubwa kuliko hizi, maana mimi nakwenda kwa Baba. Tena lo lote, mtakaloliomba katika Jina langu, nitalifanya, Baba apate kutukuzwa, kwa kuwa yumo mwake Mwana. Mtakaloniomba katika Jina langu, nitalifanya. *Mkinipenda yashikeni maagizo yangu! Nami nitamwomba Baba, naye atawapa mtuliza mioyo mwingine, akae pamoja nanyi kale na kale. Ndiye Roho wa kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni, wala haumtambui. Ninyi mnamtambua, kwani anakaa kwenu, naye atakuwamo mwenu. Sitawaacha peke yenu, nitakuja kwenu. Bado kidogo ulimwengu hautaniona tena, lakini ninyi mtaniona, kwani mimi nipo ninaishi, nanyi mtakuwa mnaishi. Siku ile mtatambua ninyi, ya kuwa mimi nimo mwake Baba yangu, nanyi mmo mwangu, nami nimo mwenu. Aliye na maagizo yangu, akiyashika, huyo ndiye mwenye kunipenda. Lakini mwenye kunipenda atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda nimwonyeshe, nilivyo.* Yuda, lakini siye Iskariota, akamwambia: Bwana, imekuwaje, ukitaka kutuonyesha sisi, ulivyo, usipovionyesha wao wa ulimwengu? *Yesu akajibu, akamwambia: Mtu akinipenda atalishika Neno langu, naye Baba yangu atampenda, nasi tutamfikia, tufanye makao kwake. Asiyenipenda hayashiki maneno yangu; nalo Neno, mnalolisikia, silo langu, ila la Baba aliyenituma. Haya nimewaambia nikingali kwenu. Lakini yule mtuliza mioyo, yule Roho Mtakatifu, Baba atakayemtuma katika Jina langu, ndiye atakayewafundisha yote na kuwakumbusha yote, mimi niliyowaambia ninyi. Nawaachia utengemano, utengemano wangu nawapani. Mimi siwapi, kama ulimwengu unavyowapa. Mioyo yenu isizizimke, wala isiogope! Mmesikia, nilivyowaambia: Nakwenda zangu, tena nitawajia. Kama mngenipenda, mngefurahi, ya kuwa nakwenda kwa Baba, kwani Baba ni mkubwa kuliko mimi. Sasa nimewaambia, yanapokuwa hayajafanyika bado, mpate kunitegemea, yatakapofanyika. Sitasema nanyi mengi tena, kwani mtawala ulimwengu huu anakuja; lakini hakuna tena, anachokiweza kwangu mimi, ni kwamba tu, ulimwengu upate kutambua, ya kuwa nampenda Baba, nikafanya hivyo, Baba alivyoniagiza., Inukeni, tutoke humu!* *Mimi ni mzabibu wa kweli naye Baba yangu ndiye mpalilizi. Kila tawi langu lisilozaa huliondoa; lakini kila tawi lizaalo hulitakasa akilipogoa, lipate kuzaa mengi. Ninyi mmekwisha kutakata mkilipokea lile Neno, nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu! Kama tawi lisivyoweza kuzaa likiwa peke yake, lisipokaa mzabibuni, vivyo hivyo nanyi hamna mwezacho, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu, ninyi m matawi. Anayekaa ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa mengi. Kwani pasipo mimi hamna mwezacho kukifanya. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi, likikauka; kisha watu huyakusanya pamoja na kuyatupa motoni yateketee. Mtakapokaa ndani yangu, nayo maneno yangu yatakapokaa ndani yenu, mtaomba lo lote, mnalolitaka, kisha mtalipata. Hapo ndipo, Baba yangu anapotukuzwa, mnapozaa mengi, mkawa wanafunzi wangu.* *Kama Baba alivyonipenda, ndivyo, nami ninavyowapenda ninyi. Kaeni na kunipenda! Mtakapoyashika maneno yangu mtakaa na kunipenda, kama mimi nilivyoyashika maagizo ya Baba yangu, nikakaa na kumpenda yeye. Nimewaambia haya, furaha yangu iwakalie, nanyi furaha yenu itimie yote. Hili ndilo agizo langu: Mpendane, kama nilivyowapenda! Hakuna mwenye upendo kumpita mwenye kujitoa, awaokoe wapenzi wake. Ninyi m wapenzi wangu mkiyafanya, ninayowaagiza. Sitawaita tena watumwa, kwani mtumwa hayajui, bwana wake anayoyafanya. Nimewaita wapenzi, kwani yote, niliyoyasikia kwa Baba yangu, nimewatambulisha ninyi. Sio ninyi mlionichagua, lakini ndiye mimi niliyewachagua ninyi, nikawaweka, mwende kuzaa matunda, nayo matunda yenu yakae; kwa hiyo Baba atawapa lo lote, mtakalomwomba katika Jina langu.* Haya nawaagizani: Mpendane! Ulimwengu ukiwachukia, tambueni, ya kuwa mimi ni mtangulizi wenu aliyeanza kuchukiwa nao! Kama mngekuwa wa ulimwengu, wao wa ulimwengu wangewapenda, kwamba m wenzao. Lakini kwa sababu ham wa ulimwengu, kwani mimi naliwachagua na kuwatoa ulimwenguni, kwa hiyo wao wa ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno, nililowaambia: Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake! Kama wamenifukuza mimi, watawafukuza nanyi. Kama wamelishika Neno langu, hata lenu watalishika. Lakini hayo yote watawafanyia kwa ajili ya Jina langu, kwani hawamjui aliyenituma. Kama singalikuja na kusema nao, wasingalikuwa na kosa; lakini sasa hawana, watakalojikania makosa yao. Mwenye kunichukia mimi humchukia naye Baba yangu. Kama singalifanya kwao kazi, mwingine asizozifanya hata kale, wasingalikuwa na kosa. Lakini sasa wameziona, kisha wametuchukia, mimi na Baba yangu. Lakini sharti litimie neno lililoandikwa katika Maonyo yao ya kwamba: Walinichukia bure. *Lakini atakapokuja mtuliza mioyo, nitakayemtuma toka kwa Baba, yule Roho wa kweli atakayetoka kwa Baba, ndiye atakayenishuhudia. Lakini nanyi m mashahidi, kwani tangu mwanzo mlikuwa pamoja nami. Haya nimewaambia, maana msije kukwazwa. Watawakataza kuziingia nyumba za kuombea; kweli saa inakuja, kila mwenye kuwaua ninyi atakapodhani, ya kuwa anamtumikia Mungu. Hivyo watavifanya, kwa sababu hawakumtambua Baba wala mimi. Lakini nimewaambia haya, kwamba saa yao itakapokuja, myakumbuke, ya kuwa mimi nimewaambia ninyi. Lakini tangu mwanzo sikuwaambia haya kwa hivyo, nilivyokuwa pamoja nanyi.* *Lakini sasa nakwenda kwake yeye aliyenituma, tena kwenu hakuna anayeniuliza: Unakwenda wapi? Ila kwa sababu nimewaambia haya, mioyo yenu imejaa masikitiko. Lakini mimi nawaambiani lililo la kweli: Inawafalia, mimi niende zangu. Kwani nisipokwenda zangu, mtuliza mioyo hatawajia. Lakini nitakapokwenda, nitamtuma kwenu. Naye atakapokuja atawaumbua wao wa ulimwengu kuwa wenye makosa wasio nalo la kujikania, wanaopaswa na kuhukumiwa. Ndio wenye makosa, kwa kuwa hawanitegemei mimi; hawana la kujikania, kwa kuwa nakwenda kwa Baba, nanyi hamnioni tena; wapaswa na kuhukumiwa, kwa kuwa mtawala ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa. Yako maneno mengi bado, ninayotaka kuwaambia; lakini sasa mngeyaona kuwa mzigo usiochukulika. Lakini yule atakapokuja, yule Roho wa kweli, yeye atawaongoza, awapeleke penye yote yaliyo ya kweli. Kwani hatayasema maneno yake mwenyewe, ila atayasema, atakayoyasikia, awatangazie nayo yatakayokuja. Yeye ndiye atakayenitukuza, kwani katika yale yaliyo yangu ndimo, atakamoyatwaa, atakayowatangazia ninyi. Yote, Baba aliyo nayo, ni yangu; kwa hiyo nilisema: Katika yale yaliyo yangu ndimo, atakamoyatwaa, atakayowatangazia ninyi.* *Bado kidogo hamtaniona; tena patakapopita kitambo kidogo, mtaniona tena, kwa sababu ninakwenda kwa Baba. Basi, kulikuwako wanafunzi wake waliosemezana wao kwa wao: Neno hili, analotuambia, ni neno gani la kwamba: Bado kidogo hamtaniona, tena patakapopita kidogo, mtaniona? Na tena: Ninakwenda kwa Baba? Wakasema: Lile bado kidogo, alisemalo, ni kusemaje? Hatujui, analosema. Kwa kuwatambua, ya kuwa walitaka kumwuliza, Yesu akawaambia: Mnaulizana kwa hilo, nililolisema: Bado kidogo hamtaniona; tena patakapopita kidogo, mtaniona? Kweli kweli nawaambiani: Ninyi mtalia na kuomboleza, lakini wao wa ulimwengu watafurahi. Ninyi mtasikitika, lakini sikitiko lenu litageuka kuwa furaha. Mwanamke anapozaa husikitika, kwani saa yake imekuja; lakini akiisha kumzaa mwana hayakumbuki tena maumivu, ila hufurahi kwa ajili ya mtu aliyezaliwa kukaa ulimwenguni. Basi, nanyi sasa mnasikitika, lakini tutaonana tena, ndipo, mioyo yenu itakapofurahi; hiyo furaha yenu hakuna atakayeiondoa kwenu. Siku ile hamtaniuliza neno.* *Kweli kweli nawaambiani: Lo lote, mtakalomwomba Baba, atawapa katika Jina langu. Mpaka leo hakuna, mliloliomba katika Jina langu. Ombeni! Ndipo, mtakapopewa, furaha yenu iwe imetimizwa yote! Haya nimewaambia kwa mifano. Lakini saa inakuja, itakapokuwa, nisiseme nanyi tena kwa mifano, ila nitawatolea waziwazi mambo ya Baba. Siku ile mtaomba katika Jina langu, nani siwaambii: Mimi nitawaombea ninyi kwake Baba. Kwani Baba mwenyewe anawapenda, kwa sababu ninyi mmenipenda mimi na kunitegemea kwamba: Mimi nimetoka kwa Baba. Nimetoka kwa Baba, nikaingia ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu, niende kwa Baba. Ndipo, wanafunzi wake waliposema: Tazama, sasa unasema waziwazi, usiseme mfano wo wote. Sasa tunajua, ya kuwa unayajua yote, ya kuwa huulizwi na mtu. Kwa hiyo tunakutegemea, ya kuwa umetoka kwa Mungu. Yesu akawajibu: Sasa mnanitegemea? Tazameni, saa inakuja, tena imekwisha fika, mtawanyike kila mtu na kwao kwenyewe, mniache mimi, niwe peke yangu. Lakini mimi sipo peke yangu, kwani Baba yupo pamoja nami. Haya nimewaambia, mpate kutengemana mwangu. Ulimwenguni mnayo maumivu; lakini tulieni mioyo! Mimi nimeushinda ulimwengu.* Yesu alipokwisha kuyasema haya akayaelekeza macho yake mbinguni, akasema: Baba, saa imekwisha fika. Mtukuze Mwana wako, Mwana wako naye akutukuze! Ni kama hivyo, ulivyompa kumtawala kila mwenye mwili, awape wote, uliompa, uzima wa kale na kale. Nao huu ndio uzima wa kale na kale, wakutambue wewe, kwamba ndiwe peke yako Mungu wa kweli, tena wamtambue yule, uliyemtuma, kwamba ndiye Yesu Kristo. Mimi nimekutukuza nchini na kuitimiza kazi, uliyonipa ya kuifanya. Sasa, Baba, unitukuze kwako wewe na kunipa utukufu, niliokuwa nao nilipokuwa kwako, ulimwengu ulipokuwa haujawa bado. Jina lako nimewafumbulia watu, ulionipa na kuwatoa ulimwenguni. Walikuwa wako, nawe umenipa mimi, nalo Neno lako wamelishika. Sasa wametambua, ya kuwa yote, uliyonipa, yametoka kwako. Kwani yale maneno, uliyonipa, nimewapa, wakayapokea, wakatambua kweli, ya kuwa nilitoka kwako, wakanitegemea, ya kuwa wewe ndiwe uliyenituma. Mimi nawaombea hao, siuombei ulimwengu, ila nawaombea wale tu, ulionipa, kwani ni wako. Nayo yote yaliyo yangu ni yako, nayo yaliyo yako ni yangu; namo mwao ndimo, nilimotukuzwa. Nami simo tena ulimwenguni, lakini wao wamo ulimwenguni, kwani mimi nakuja kwako. Baba Mtakatifu, walinde, wakae na Jina lako, ulilonipa, wapate kuwa mmoja wote, kama sisi tulivyo mmoja! Nilipokuwa pamoja nao naliwalinda, wakae na Jina lako, ulilonipa, nikawaangalia. Nao hawakuangamia hata mmoja wao, pasipo yule mwana wa mwangamizo, yaliyoandikwa yapate kutimia. Lakini kwa kuwa sasa nakuja kwako, nayasema haya ulimwenguni, waipate furaha yangu, iwajie yote. Mimi nimewapa Neno lako, ulimwengu ukawachukia, kwa sababu wao sio wa ulimwengu, kama mimi nisivyokuwa wa ulimwengu. Siombi, uwaondoe ulimwenguni, ila naomba, uwalinde, yule Mbaya asiwajie. Wao sio wa ulimwengu, kama mimi nisivyokuwa wa ulimwengu. Watakase, wawe wa kweli! Neno lako ndilo la kweli. Kama wewe ulivyonituma kwenda ulimwenguni, ndivyo nami nilivyowatuma kwenda ulimwenguni. Nao ndio, ninaojitakasia mwenyewe, kwamba nao wawe watu waliotakaswa kweli. Lakini si hawa tu, ninaowaombea, ila nawaombea hata wale watakaonitegemea wakilisikia neno lao. Wote wapate kuwa mmoja, kama ulivyomo mwangu, wewe Baba, nami nilivyomo mwako! Wapate kuwamo mwetu nao hao, ulimwengu upate kunitegemea, ya kuwa wewe umenituma. Nami nimewapa utukufu, ulionipa wewe, wapate kuwa mmoja, kama sisi tulivyo mmoja. Mimi niwemo mwao, nawe wewe uwemo mwangu, wawe watu waliomaliza kuwa mmoja, nao ulimwengu utambue, ya kuwa wewe umenituma, kisha umewapenda, kama ulivyonipenda mimi. Baba, nataka hata wale, ulionipa, wawe pamoja nami papo hapo, nitakapokuwapo mimi, wapate kuuona utukufu wangu, ulionipa, kwa sababu umenipenda, ulimwengu ulipokuwa haujaumbwa bado. Baba mwongofu, ulimwengu haukukutambua, lakini mimi nimekutambua, nao hao wametambua, ya kuwa wewe umenituma. Nami nimewatambulisha Jina lako, na tena nitalitambulisha, kwamba upendo, wewe ulionipenda, uwakalie, nami niwemo mwao. Yesu alipokwisha kuyasema haya akatoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng'ambo ya kijito cha Kidoroni, kulikokuwa na kiunga. Humo wakaingia yeye na wanafunzi wake. Lakini naye Yuda aliyemchongea alipajua hapo, kwani Yesu na wanafunzi wake walikusanyika mara nyingi hapo. Basi, Yuda alipokwisha kupata kikosi cha askari na watumishi wa watambikaji wakuu na wa Mafariseo, akaenda kulekule, wakishika taa na mienge na selaha. Yesu alipoyajua yote yatakayomjia akawatokea, akawauliza: Mwamtafuta nani? Walipomjibu: Yesu wa Nasareti, akawaambia: Ni mimi. Lakini naye Yuda mwenye kumchongea alikuwa amesimama pamoja nao. Alipowaambia: Ni mimi, wakarudi nyuma, wakaanguka chini. Alipowauliza tena: Mwamtafuta nani? wakasema: Yesu wa Nasareti. Yesu akajibu: Nimekwisha waambia: Ni mimi; mkinitafuta mimi, waacheni hawa, waende zao! Imekuwa hivyo, litimie lile neno, alilolisema: Wale, ulionipa, sikuwaangamiza hata mmoja. Simoni Petero alikuwa na upanga, akauchomoa, akampiga mtumwa wa mtambikaji mkuu, akamkata sikio la kuume; jina lake yule mtumwa ndiye Malko. Lakini Yesu akamwambia Petero: Uchomeke upanga alani mwake! Kinyweo, Baba alichonipa, nisikinywe? Kisha kikosi cha askari na mkubwa wao na watumishi wa Wayuda wakamkamata Yesu, wakamfunga. Wakampeleka kwanza kwa Ana; kwani alikuwa mkwewe Kayafa aliyekuwa mtambikaji mkuu wa mwaka ule. Kayafa ndiye yule aliyekula njama na Wayuda kwamba: Inafaa, mtu mmoja afe kwa ajili ya watu. Lakini Simoni Petero na mwanafunzi mwingine wakamfuata Yesu; yule mwanafunzi mwingine alikuwa amejuana na mtambikaji mkuu, akaingia pamoja na Yesu uani kwa mtambikaji mkuu, Petero akasimama nje mlangoni. Yule mwanafunzi mwingine aliyejuana na mtambikaji mkuu akatoka, akasema na mlinda mlango, akamwingiza Petero. Kisha kijakazi aliyekuwa mlinda mlango alipomwambia Petero: Wewe nawe humo miongoni mwao wanafunzi wa mtu huyo? akasema: Simo. Lakini watumwa na watumishi walikuwa wamewasha moto wa makaa, kwani palikuwa na baridi, wakasimama, wakaota moto; naye Petero alisimama pamoja nao, akiota moto. Mtambikaji mkuu alipomwuliza Yesu kwa ajili ya wanafunzi wake na kwa ajili ya mafundisho yake, Yesu akamjibu: Mimi nimesema waziwazi ulimwenguni. Mimi siku zote nimefundisha nyumbani mwa kuombea napo Patakatifu, Wayuda wote wanapokusanyika; hakuna, nililolisema na kufichaficha, Unaniulizaje? Uwaulize walionisikia, niliyowaambia! Tazama, hao wanayajua, niliyoyasema mimi. Aliposema hivyo, mtumishi mmoja aliyesimama hapo akampiga Yesu kofi akisema: Mtambikaji mkuu unamjibu hivyo? Yesu akamjibu: Kama nimesema maovu, ujulishe huo uovu! Lakini kama nimesema vema, unanipigia nini? Basi, Ana akampeleka kwa mtambikaji mkuu Kayafa hivyo, alivyokuwa amefungwa. Lakini Simoni Petero alikuwa amesimama akiota moto. Walipomwuliza: Wewe nawe humo miongoni mwao wanafunzi wake? akakana akisema: Simo. Miongoni mwao watumwa wa mtambikaji mkuu mlikuwamo mmoja aliyekuwa ndugu yake yule, Petero aliyemkata sikio, akasema: Mimi sikukuona kule kiungani pamoja naye? Petero akakana tena; mara hiyo jogoo akawika. Wakamtoa Yesu kwa Kayafa, wakampeleka bomani kulipokucha. Wao wenyewe hawakuingia bomani kwa mwiko wao, wasijitie uchafu, wapate kula Pasaka. Kwa hiyo Pilato akawatokea nje, akauliza: Mwaleta mashtaka gani ya mtu huyu? Walipojibu wakimwambia: Huyu kama asingekuwa mwenye kufanya maovu, tusingemleta kwako, Pilato akawaambia: Mchukueni ninyi, mmhukumu kwa Maonyo yenu! Wale Wayuda wakamwambia: Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu. Ilikuwa hivyo, litimie lile neno, Yesu alilolisema na kuonyesha kufa kulikomngoja. Pilato akaingia tena bomani, akamwita Yesu, akamwuliza: Wewe ndiwe mfalme wa Wayuda? Yesu akajibu: Wasema hivi kwa mawazo yako mwenyewe, au wako wengine waliokusimulia mambo yangu? Pilato akajibu: Je? Mimi Myuda? Wao wa taifa lako na watambikaji wakuu wamekuleta kwangu. Umefanya nini? Yesu akajibu: Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangeupigania, nisitiwe mikononi mwa Wayuda. Lakini sasa ufalme wangu sio wa hapa. Pilato akamwuliza: Basi, wewe u mfalme gani? Yesu akajibu: Wewe unavyosema, ndivyo: mimi ni mfalme. Niliyozaliwa, tena niliyojia ulimwenguni, ndiyo hii: niishuhudie iliyo ya kweli! Kila aliye na kweli huisikia sauti yangu. Pilato akamwambia: Iliyo ya kweli ndiyo nini? Alipokwisha kuyasema haya akawatokea tena Wayuda, akawaambia: Mimi sioni kwake neno la kumhukumu. Lakini iko desturi kwenu, niwafungulie mmoja siku ya Pasaka; basi, mwataka, niwafungulie mfalme wa Wayuda? Ndipo, walipopiga makelele tena wakisema: Huyu hatumtaki, twamtaka Baraba; naye Baraba alikuwa mnyang'anyi. Ndipo, Pilato alipomchukua Yesu, akampiga viboko. Kisha askari wakasuka kilemba cha miiba, wakamvika kichwani, wakamvika hata nguo ya kifalme, wakamjia wakisema: Pongezi, mfalme wa Wayuda! wakampiga makofi. Pilato alipotoka tena nje, akawaambia: Tazameni, ninampeleka kwenu nje, mpate kutambua, ya kuwa sioni kwake neno la kumhukumu. Yesu akatoka nje, amekivaa kilemba cha miiba na nguo ya kifalme. Pilato akawaambia: Mtazameni mtu huyu! Watambikaji wakuu na watumishi walipomwona wakapiga makelele wakisema: Mwambe msalabani! Mwambe msalabani! Pilato alipowaambia: Mchukueni ninyi, mmwambe msalabani! Kwani mimi sioni kwake neno la kumhukumu. Wayuda wakamjibu: Sisi tuko na Maonyo, kwa Maonyo hayo sharti afe, kwani amejifanya kuwa Mwana wa Mungu. Pilato alipolisikia neno hili akakaza kuogopa, akaingia tena bomani, akamwuliza Yesu: Umetoka wapi? Lakini Yesu hakumjibu neno. Pilato alipomwambia: Husemi na mimi? Hujui, ya kuwa nina nguvu ya kukufungua na nguvu ya kukuwamba msalabani? Yesu akajibu: Hungekuwa na nguvu ya kunihukumu, kama usingepewa toka juu. Kwa hiyo yule aliyenitia mikononi mwako yuko na kosa linalolipita lako. Toka hapo Pilato alitafuta njia ya kumfungua. Lakini Wayuda wakapiga makelele wakisema: Unapomfungua huyu hu mpenzi wake Kaisari. Kila mwenye kujifanya kuwa mfalme humkataa Kaisari. Pilato alipoyasikia maneno haya akampeleka Yesu nje, akaketi katika kiti cha uamuzi mahali panapoitwa Kiwanja cha Mawe, lakini Kiebureo: Gabata. Lakini ilikuwa siku ya kuandalia Pasaka kama saa sita; alipowaambia Wayuda: Mtazameni mfalme wenu! wale wakapiga makelele: Mwondoe! Mwondoe! Mwambe msalabani! Pilato alipowaambia: Nimwambe mfalme wenu msalabani? watambikaji wakuu wakajibu: Hatuna mfalme pasipo Kaisari. Basi, hapo ndipo, alipomtoa, awambwe msalabani. Wakampeleka Yesu; naye akajichukulia mwenyewe msalaba wake alipotoka kwenda mahali panapoitwa Fuvu la Kichwa, jina lake Kiebureo: Golgota. Ndipo, walipomwamba msalabani; tena pamoja naye wakawamba misalabani wengine wawili, huku na huko, lakini Yesu katikati. Pilato akaandika mwandiko, akaubandika msalabani juu; hapo palikuwa pameandikwa: YESU WA NASARETI, MFALME WA WAYUDA. Mwandiko huo Wayuda wengi waliusoma, kwani mahali pale, Yesu alipowambwa msalabani, palikuwa karibu na mji. Nao ulikuwa umeandikwa Kiebureo na Kiroma na Kigriki. Watambikaji wakuu wa Wayuda walipomwambia Pilato: Usiandike: Mfalme wa Wayuda, ila: Huyu amesema: Mimi ni mfalme wa Wayuda! Pilato akajibu: Niliyoyaandika, basi, nimekwisha kuyaandika. Askari walipokwisha kumwamba Yesu msalabani wakayachukua mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kila askari fungu moja, wakaichukua hata kanzu. Lakini ile kanzu ilikuwa pasipo mshono, toka juu yote ilikuwa imefumwa tu. Kwa hiyo wakaambiana: Tusiipasue, ila tuipigie kura, ajulike atakayeipata. Imekuwa hivyo, litimie lililoandikwa: Wakajigawanyia nguo zangu, nalo vazi langu zuri wakalipigia kura. Ndio askari waliofanya hivyo. Lakini penye msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama akina mama yake na ndugu ya mama yake, jina lake Maria wa Klofa, na Maria Magadalene. Yesu alipomwona mama yake na yule mwanafunzi, aliyempenda, akisimama karibu, akamwambia mama yake: Mama, tazama, mwana wako huyu! Kisha akamwambia yule mwanafunzi: Tazama, mama yako huyu! Tokea saa ileile yule mwanafunzi akamchukua, akampeleka nyumbani mwake. Baadaye Yesu alipojua, ya kuwa yote yamekwisha timizwa, akasema: Nina kiu, kwamba nayo hayo yaliyoandikwa yapate kutimia. Palikuwa pamewekwa chombo kilichojaa siki. Basi, wakachukua mwani, wakauchovya sikini, wakautia katika kivumbasi, wakampelekea kinywani. Yesu alipokwisha pewa ile siki, akasema: Yamemalizika. Kisha akainama kichwa, akakata roho. Kwa Wayuda siku ile ilikuwa ya kuandalia Pasaka, kwa hiyo wakamwomba Pilato, miguu yao waliowambwa misalabani ivunjwe, waondolewe, miili yao isikae misalabani siku ya mapumziko, kwani siku ile ya mapumziko ilikuwa kuu. Wakaja askari, wakawavunja miguu wa kwanza na wa pili, waliowambwa misalabani pamoja naye. Lakini walipofika kwa Yesu, wakiona, ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; ila askari mmoja akamchoma mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji. Yeye aliyeyaona hayo ameyashuhudia, nao ushuhuda wake ni wa kweli, naye anajua, ya kuwa anasema kweli, nanyi mpate kuyasadiki. Kwani hayo yalikuwa, yatimie yaliyoandikwa: Hakuna mfupa wake utakaovunjwa. Tena liko neno jingine lililoandikwa la kwamba: Watamtazama yule, waliyemchoma. Hayo yalipokwisha, akatokea Yosefu wa Arimatia aliyekuwa mwanafunzi wa Yesu, lakini alikuwa amejifichaficha kwa kuwaogopa Wayuda; yeye ndiye aliyemwomba Pilato ruhusa ya kuuondoa mwili wa Yesu. Pilato alipompa ruhusa, akaenda, akauondoa mwili wake. Pakaja Nikodemo naye, ni yule aliyemjia usiku hapo kwanza, akaleta manemane iliyochanganyika na uvumba, yapata kama mizigo miwili. Kisha wakautwaa mwili wa Yesu, wakaufunga kwa sanda pamoja na yale manukato, kama Wayuda walivyozoea kuzika. Mahali pale, alipowambwa msalabani palikuwa na kiunga, namo mle kiungani mlikuwa na kaburi jipya, ambalo hajazikwa mtu bado ndani yake. Kwa sababu ni siku ya kuandalia kwa Wayuda, wakamweka Yesu mle, kwani lile kaburi lilikuwa karibu. Siku ya kwanza ya juma Maria Magadalene akaenda mapema kaburini, kukingali gizagiza. Alipoliona lile jiwe, limekwisha ondolewa kaburini, akapiga mbio, akamwendea Simoni Petero na yule mwanafunzi mwingine, Yesu aliyempenda, akawaambia: Wamemwondoa Bwana kaburini, nasi hatujui, walikomweka. Ndipo, Petero na yule mwanafunzi mwingine walipoondoka kwenda kaburini, wote wawili wakipiga mbio pamoja; lakini yule mwanafunzi mwingine akaja mbele kwa mbio, akamshinda Petero, akafika wa kwanza penye kaburi. Akainama, akachungulia, akaiona sanda, imewekwa, lakini hakuingia. Kisha Simoni Petero akafika akimfuata, akaingia kaburini, akaiona sanda, imewekwa; lakini mharuma uliokuwa kichwani pake haukuwekwa pamoja na sanda, ila ulikuwa umekunjwa na kuwekwa mahali pake peke yake. Ndipo, alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyefika wa kwanza penye kaburi, akaviona, akavisadiki. Kwani hawajayajua bado yaliyoandikwa kwamba: Imempasa kufufuka katika wafu. Kisha wale wanafunzi wakarudi tena kwao. *Lakini Maria alikuwa amesimama nje penye kaburi akilia. Basi, alipokuwa akilia, akainama kuchungulia kaburini, akaona malaika wawili wenye nguo nyeupe, wamekaa hapo, mwili wa Yesu ulipokuwa umewekwa, mmoja kichwani, mmoja miguuni. Hao walipomwuliza: Mama, waliliani? akawaambia: Maana wamemwondoa Bwana wangu, nami sijui, walikomweka. Alipoyasema hayo akageuka nyuma, akamwona Yesu, amesimama, lakini hakujua, ya kuwa ndiye Yesu. Yesu alipomwambia: Mama, waliliani? Wamtafuta nani? alidhani, ni mlinzi wa kiunga, akamwambia: Bwana, kama wewe umemchukua, niambie, ulikomweka, nipate kwenda, nimchukue! Yesu akamwambia: Maria! Ndipo, alipogeuka, akamwambia Kiebureo: Rabuni! maana yake: Mfunzi mkuu! Yesu akamwambia: Usiniguse! Kwani sijapaa bado kwenda kwake Baba. Lakini uende kwa ndugu zangu, uwaambie: Ninapaa kwenda kwa Baba yangu aliye hata Baba yenu na kwa Mungu wangu aliye hata Mungu wenu. Maria Magadalene akaenda, akawasimulia wanafunzi: Nimemwona Bwana, tena hayo ndiyo, aliyoniambia.* *Siku ile ya kwanza ya juma kulipokuchwa, wanafunzi wakakutana, milango ya mle walimokuwa ikiwa imefungwa, maana waliwaogopa Wayuda. Mara Yesu akaja, akasimama katikati, akawaambia: Tengemaneni! Naye alipokwisha kuyasema haya akawaonyesha maganja na ubavu. Wanafunzi walipomwona Bwana wakafurahi. Yesu akawaambia tena: Tengemaneni! Kama Baba alivyonituma mimi, ndivyo, nami ninavyowatuma ninyi. Naye alipokwisha kuyasema haya, akawapuzia, akawaambia: Pokeeni Roho takatifu! Watu, mtakaowaondolea makosa, watakuwa wameondolewa. Nao watu, mtakaowafungia, watakuwa wamefungiwa. Lakini Toma anayeitwa Pacha aliyekuwa mmoja wao wale kumi na wawili hakuwamo pamoja nao, Yesu alipokuja. Wanafunzi wenzake walipomwambia: Tumemwona Bwana! akawajibu: Nisipoyaona makovu ya misumari maganjani mwake na kukitia kidole changu pale penye misumari, tena nisipoutia mkono wangu ubavuni mwake, sitamtegemea. Baada ya siku nane wanafunzi wake walikuwamo tena, naye Toma alikuwa yumo pamoja nao. Yesu akaja, milango ilipokuwa imefungwa, akasimama katikati, akasema: Tengemaneni! Kisha akamwambia Toma: Lete kidole chako hapa, uyatazame maganja yangu! Lete nao mkono wako, uutie ubavuni mwangu! Usiwe mtu asiyenitegemea, ila anitegemeaye! Ndipo, Toma alipomjibu, akamwambia: Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia: Umenitegemea, kwa sababu umeniona. Wenye shangwe ndio wanitegemeao pasipo kuona! Viko vielekezo vingi vingine, Yesu alivyovifanya mbele ya wanafunzi, visivyoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hivyo vimeandikwa, mpate kuyategemea, ya kuwa Yesu ndiye Kristo, Mwana wake Mungu, tena mpate uzima katika Jina lake kwa kumtegemea.* Kisha Yesu akajijulisha tena kwa wanafunzi kwenye bahari ya Tiberia. Alivyojijulisha ni hivyo: walikuwako pamoja Simoni Petero na Toma anayeitwa Pacha na Natanaeli wa Kana wa Galilea na wana wa Zebedeo na wanafunzi wake wengine wawili. Simoni Petero alipowaambia: Nakwenda kuvua, wakamwambia: Nasi tunakwenda pamoja na wewe. Basi, wakaondoka, wakaingia chomboni, lakini usiku ule hawakupata kitu. Kulipoanza kucha, Yesu alikuwa amesimama ufukoni, lakini wanafunzi hawakumjua, ya kuwa ndiye Yesu. Yesu alipowauliza: Wanangu, hamna kitoweo? wakamjibu: Hatuna. Ndipo, alipowaambia: Utupeni wavu kuumeni kwa chombo, ndiko, mtakakopata! Walipoutupa, tena hawakuweza kuuvuta kwa ajili ya samaki wengi. Ndipo, yule mwanafunzi, Yesu aliyempenda, alipomwambia Petero: Ni Bwana! Simoni Petero aliposikia, ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi, kwani alikuwa uchi, akajitupa baharini. Wanafunzi wenziwe wakaenda kwa chombo wakiuvuta wavu uliojaa samaki, kwani pwani hapakuwapo mbali, palikuwa kama mikono 200 tu. Nao waliposhuka pwani wakaona: moto wa makaa ulikuwa umewashwa, navyo visamaki vilikuwa vimewekwa juu pamoja na mkate. Yesu akawaambia: Leteni kidogo katika visamaki hivyo, mlivyovivua sasa hivi! Simoni Petero akapanda chomboni, akauvuta wavu ufukoni; wakawamo samaki wakubwa tu 153. Nao wavu haukupasuka, wangawa wengi kama hao. Kisha Yesu akawaambia: Njoni, mle! Miongoni mwao hao wanafunzi hakuwamo hata mmoja aliyejipa moyo wa kumwuliza: Wewe u nani? Walimjua, ya kuwa ndiye Bwana. Kisha Yesu akaenda, akautwaa mkate, akawagawia, na kitoweo vilevile. Hii ndiyo mara ya tatu, Yesu akijijulisha kwa wanafunzi alipokwisha fufuka katika wafu. *Walipokwisha kula, Yesu akamwuliza Simoni Petero: Simoni wa Yohana, wanipenda kuliko hawa? Akamwambia: Ndio, Bwana, wewe unajua, ya kuwa ninakupenda. Akamwambia: Walishe wana kondoo wangu! Alipomwuliza tena mara ya pili: Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia: Ndio, Bwana, wewe unajua, ya kuwa ninakupenda. Akamwambia: Vichunge vikondoo vyangu! Alipomwuliza mara ya tatu: Simoni wa Yohana, Wanipenda? Petero akasikitika, kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: Wanipenda? akamwambia: Bwana, wewe unayajua yote, wewe unatambua, ya kuwa ninakupenda. Yesu akamwambia: Vilishe vikondoo vyangu! Kweli kweli nakuambia: Ulipokuwa kijana ulijifunga mwenyewe, ukaenda, ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utainyosha mikono yako, mwingine akuvike, akupeleke, usikotaka. Neno hili alilisema, amwonyeshe kufa, alikotakiwa, amtukuze Mungu nako. Alipokwisha kuyasema haya akamwambia; Nifuate!* Petero alipogeuka akaona, anafuata naye yule mwanafunzi, Yesu aliyempenda, ni yule aliyekuwa ameegamia kifuani pake, walipokuwa wakila jioni, aliyemwuliza: Bwana, ni nani, atakayekuchongea? Basi, Petero alipomwona huyu akamwuliza Yesu: Bwana, na huyu je? Yesu akamwambia: Nikitaka, huyu akae, mpaka nitakapokuja, wewe unavikataliaje? Wewe nifuate tu! Basi, neno hili likaenea katika ndugu la kwamba: Mwanafunzi huyu hatakufa. Lakini Yesu hakumwambia: Hatakufa, ila: Nikitaka, huyu akae, mpaka nitakapokuja, wewe unavikataliaje? Huyu ndiye mwanafunzi aliyeyashuhudia haya na kuyaandika. Nasi twamjua, ya kuwa ushuhuda wake ni wa kweli. Lakini yako hata mengine mengi, Yesu aliyoyafanya. Nayo kama yangaliandikwa moja moja, nadhani, ulimwengu wote usingevitoshea vitabu vitakavyoandikwa. *Mwenzangu Teofilo, katika kitabu cha kwanza nalikuandikia yote, Yesu aliyoanza kuyafanya na kuyafundisha mpaka siku ile, alipopazwa mbinguni. Hapo alikuwa amekwisha kuwaagizia mitume, aliowachagua, mambo ya Roho takatifu. Tena wale ndio, aliowatokea na kuwaonyesha mara kwa mara, ya kuwa anaishi, alipokuwa amekwisha kuteswa; zile siku za kuwaonekea na kusema nao mambo ya ufalme wa Mungu zilikuwa 40. Alipokwisha kuwakusanya akawaagiza, wasitoke Yerusalemu, ila wakingoje kiagio cha Baba, mlichokisikia kwangu; kwani Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho takatifu, tena siku hizo zinazosalia ni chache tu. Waliokusanyika walipomwuliza: Bwana, siku hizo ndipo, utakapowasimamishia Waisiraeli ufalme wao tena? akawaambia: Si nyie waliopaswa na kutambua siku au saa, Baba alizoziweka kwa nguvu yake yeye; ila mtapewa nguvu, Roho Mtakatifu atakapowashukia ninyi, kisha mtakuwa mashahidi wangu hapa Yerusalemu na katika nchi yote ya Yudea na ya Samaria, mfike hata mapeoni kwa nchi. Naye alipokwisha kuyasema haya akainuliwa juu, wakitazama, wingu lilivyomchukua machoni pao. Walipokuwa wakitumbuliza macho mbinguni, alikokwenda, mara waume wawili wenye nguo nyeupe wakasimama huko kwao, nao wakasema: Nyie waume wa Galilea, mmesimamaje mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kwenu na kupazwa mbinguni atarudi vivyo hivyo, mlivyomwona, akienda zake mbinguni.* Ndipo, walipoondoka penye huo mlima unaoitwa Wa Michekele, ulioko karibu ya Yerusalemu, ni mwendo usio na mwiko wa siku ya mapumziko; wakarudi Yerusalemu. Walipokwisha ingia wakapanda kipaani mle walimokaa, ni Petero na Yohana na Yakobo na Anderea, Filipo na Toma, Bartolomeo na Mateo, Yakobo wa Alfeo na Simon Zelote na Yuda wa Yakobo. Hao wote walishikamana na kutenda moyo mmoja wa kumwomba Mungu, wakawa pamoja na wale wanawake na Maria, mamake Yesu, na pamoja na ndugu zake. Siku zile Petero aliinuka katikati ya ndugu waliokuwa wamekutana pamoja, wapata 120, akasema: Waume ndugu zangu, ilipasa andiko litimie, Roho Mtakatifu alilolisema kale kinywani mwa Dawidi kwa ajili ya Yuda aliyekuwa kiongozi wao waliomkamata Yasu. Kwani alikuwa amehesabiwa pamoja nasi, tena huu utumishi wetu ulikuwa bia moja naye. Huyo amepata konde kwa mshahara wa upotovu, akaanguka kifudifudi, akatumbuka katikati, nayo matumbo yake yote yakatoka. Vikatambulikana kwa wenyeji wote wa Yerusalemu, wakaliita konde lile kwa msemo wao Hakeldama, ni kwamba: Konde la Damu. Kwani imeandikwa katika kitabu cha Mashangilio: Kao lake liwe hame tu, asioneke atakayetua mlemle. Tena: Mtu mwingine na autwae ukaguzi wake. Basi, wako wenzetu waliokuwa pamoja nasi siku zote, Bwana Yesu alipoingia kwetu, mpaka alipotoka tena, tangu hapo, Yohana alipobatiza, mpaka siku ile, alipopazwa na kutolewa kwetu; inapasa, mmoja wao awe shahidi wa ufufuko wake pamoja nasi. Wakasimamisha wawili: Yosefu aliyeitwa Barsaba, aliyekuwa na jina jingine la Yusto, na Matia. Kisha wakamwomba Mungu wakisema: Wewe Bwana, uitambuaye mioyo yao wote, tuonyeshe mmoja, uliyemchagua katika hawa wawili, aupokee huu utumishi na utume, apashike mahali, Yuda alipotoka, aende zake mahali pake yeye. Walipowapigia kura, kura ikamguia Matia; kwa hiyo akahesabiwa pamoja na wale mitume kumi na mmoja. Siku ya Pentekote (Hamsini) ilipotimia, wote walikuwa pamoja mahali palepale pamoja. Mara kukatoka uvumi mbinguni kama wa upepo unaovuma na nguvu, ukaijaza nyumba yote, walimokuwa wakikaa. Tena zikaonekana ndimi zilizogawanyika kama za moto, zikawakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho takatifu, wakaanza kusema kwa misemo mingine, kama Roho alivyowapa, watamke. Mle Yerusalemu walikuwamo wakikaa Wayuda wenye kumcha Mungu wa kila taifa lililoko chini ya mbingu. Ule mvumo uliposikilika, watu wengi wakakusanyika, wakashangaa, kwani kila mtu aliwasikia, wakisema msemo wake yeye. Wakastuka na kustaajabu wakisema: Kumbe hawa wote wanaosema sio Wagalilea! Tena inakuwaje, sisi kila mtu tukiisikia misemo ya kwetu sisi, tuliyozaliwa nayo? Sisi Waparti na Wamedi na Waelamu, nasi tunaokaa Mesopotamia na Yudea na Kapadokia, Ponto na Asia, Furigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia zinazoelekea Kirene, sisi Waroma tunaokaa ugenini huku, sisi tulio Wayuda nasi tulio wafuasi, Wakreta na Waarabu, twawasikia hawa, wakiyatangaza makuu yake Mungu kwa ndimi zetu! Wakastaajabu wote wakipotelewa nayo, wakaulizana wao kwa wao: Jambo hili litakwenda kuwaje? Lakini wengine wakafyoza wakisema: Wamelewa mvinyo mbichi!* Ndipo, Petero alipoinuka pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake akawaambia: Nyie waume Wayuda nanyi nyote mnaokaa Yerusalemu, jambo hili sharti litambulike kwenu, mpate kuyasikiliza maneno yangu! Kwani hawa hawakulewa, kama ninyi mnavyowawazia, maana sasa ni saa tatu ya mchana. Lakini hili ndilo lililosemwa na mfumbuaji Yoeli, ya kuwa Mungu anasema: Siku za mwisho ndipo, itakapokuwa, niwamiminie Roho yangu wote wenye miili ya kimtu. Nao wana wenu wa kiume na wa kike watasema na kufumbua, nao vijana wenu wataona maono; nao wazee wenu wataoteshwa ndoto. Nao walio watumwa wangu waume na wake nitawamiminia Roho yangu siku zilezile, nao watasema na kufumbua. Nami nitafanya vioja juu mbinguni na vielekezo chini katika nchi, vyenye damu na moto na moshimoshi. Jua litageuka, liwe giza, nao mwezi utageuka, uwe damu, mbele ya kutimia kwake ile siku ya Bwana iliyo kubwa, wanayoingoja wote. Tena itakuwa, kila atakayelitambikia Jina la Bwana, ataokoka. Enyi waume wa Kiisiraeli, yasikilizeni maneno haya! Yesu wa Nasareti alikuwa amejulikana, kwamba ametoka kwa Mungu hapo alipokuja kwenu na kufanya vya nguvu na vioja na vielekezo, tena ni Mungu aliyempa kuvifanya machoni penu, kama mnavyojua wenyewe. Kwa kuwa Mungu alikuwa amempatia kazi na kumkatia mpaka kwa vile, anavyovijua vyote, vikiwa havijatimia bado, kwa hiyo ametolewa, mkampata mikononi mwa wapotovu, mkamwua na kumwamba msalabani. Lakini Mungu akamfufua na kuufungua uchungu wa kufa, kwa sababu haikuwezekana, ashikwe kuzimuni. Kwani Dawidi anamsema: Nalimwona Bwana mbele yangu kila, nilipokuwa, kwani yuko kuumeni kwangu, nisitikisike. Kwa hiyo moyo wangu hufurahi, nao ulimi wangu hushangilia; hata mwili wangu utatulia kwa kuwa na kingojeo. Kwani hutaiacha roho yangu, ipotee kuzimuni, wala hutamtoa akuchaye, apate kuoza kaburini. Unanitambulisha njia ziendazo penye uzima, utanijaza furaha zilizopo usoni pako. Waume ndugu zangu, mnipe ruhusa, niseme kwenu waziwazi: Dawidi aliye babu yetu mkuu alikufa, akazikwa, nalo kaburi lake liko kwetu hata siku hii ya leo. Yeye kwa sababu alikuwa mfumbuaji, akajua, ya kuwa Mungu amemwapia kiapo, kwamba atatawalisha kitini pake mmoja aliye mzao wa kiunoni mwake. Hayo aliyaona mbele, yakingali nyuma bado, akayasema na kuuelekea ufufuko wake Kristo, kwani hakuachwa kuzimuni, wala mwili wake haukupata kuoza. Huyo Yesu Mungu amemfufua, nasi sote tu mashahidi wake. Naye alipokwisha kupazwa juu, akae kuumeni kwa Mungu, akapata ruhusa kwa Baba yake kukitimiza kiagio cha Roho Mtakatifu, akaimimina yiyo hiyo, ninyi mnayoiona, tena mnayoisikia. Kwani Dawidi hakupaa mbinguni, lakini anasema mwenyewe: Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti kuumeni kwangu, mpaka niwaweke adui zako chini miguuni pako! Kwa hiyo wote walio wa mlango wa Israeli watambue kweli: Huyo Yesu, mliyemwamba msalabani ninyi, Mungu amemfanya, awe Bwana na Kristo! Walipoyasikia haya wakachomwa mioyoni, wakamwambia Petero na mitume wengine: Waume ndugu zetu, tufanyeje? Petero akawajibu: Juteni, kila mmoja abatiziwe Jina lake Yesu Kristo, mwondolewe makosa yenu! Nanyi mkipate kipaji cha Roho Mtakatifu! Kwani kiagio kile ni chenu ninyi na cha watoto wenu nacho chao wote walioko mbali, Bwana Mungu wetu atakaowaita, wamjie. Sharti mwokolewe katika kizazi hiki kipotovu! Basi, waliolipokea neno lake, wakabatizwa; hivyo siku ile waligeuzwa kuwa wanafunzi watu wapata 3000. Wakaongozana na kuyashika mafundisho ya mitume, wakafanya bia ya kumegeana mkate na kuombeana kwa Mungu. Wote wakaingiwa na woga mioyoni mwao, kwani vioja na vielekezo vilivyofanywa na mitume vilikuwa vingi. Wao wote waliomtegemea Bwana walikuwa pamoja, navyo vyote wakavifanyia bia. Wakauza mali zao navyo vyote, walivyokuwa navyo, wakavigawia wote, kila mtu apate, kama alivyokosa. Kwa sababu mioyo yao ilikuwa mmoja tu, walikuwa pamoja kila siku hapo Patakatifu, wakamegeana mkate nyumba kwa nyumba wakipokea vyakula na kushangilia katika mioyo yao iliyowang'aa. Wakamsifu Mungu, wakawapendeza watu wote. Naye Bwana akawaongeza kila siku na kutia papo hapo wenye kuokoka. *Petero na Yohana wakapanda kwenda Patakatifu saa tisa, watu walipoombea. Kulikuwa na mtu aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mama yake; naye huchukuliwa, awekwe kila siku karibu ya mlango wa Patakatifu unaoitwa Mzuri, aombe sadaka kwao wanaoingia Patakatifu. Alipomwona Petero na Yohana, wakitaka kupaingia Patakatifu, akataka kupewa sadaka nao. Lakini Petero akamkazia macho pamoja na Yohana, akasema: Tutazame sisi! Alipowatumbulia macho akingoja, watakachompa, Petero akasema: Fedha na dhahabu sinazo, lakini nilicho nacho, nitakupa. Katika Jina la Yesu Kristo wa Nasareti inuka, uende! Kisha akamshika mkono wa kuume, akamwinua. Papo hapo miguu yake na fundo zake zikapata nguvu, akaruka, akasimama, akaenda, akapaingia Patakatifu pamoja nao akizunguka na kurukaruka na kumsifu Mungu. Watu wote walipomwona, anavyozunguka na kumsifu Mungu, wakamtambua, ya kuwa huyu ndiye aliyekaa na kuomba sadaka karibu ya Mlango Mzuri wa Patakatifu. Wote wakashangaa mno na kuyastukia yale yaliyompata. Aliposhikamana na Petero na Yohana, watu wote wakawakusanyikia mbio katika ukumbi unaoitwa wa Salomo kwa kushangaa. Petero alipowaona akawaambia wale watu: Waume Waisiraeli, haya mnayashangaaje? Nasi mnatutumbualiaje macho, kama ni nguvu yetu sisi, au kama ni hivyo, tunavyomcha Mungu, vinavyomwendesha huyu? Mungu wa Aburahamu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu wa kele, amemtukuza mtoto wake Yesu, ninyi mliyemtoa na kumkana mbele ya Pilato, alipokata shauri, kwamba afunguliwe. Lakini ninyi mkamkana aliyekuwa mtakatifu na mwongofu, mkataka kupewa aliyekuwa mwuaji, mwenye kuwaongoza uzimani mkamwua. Lakini Mungu amemfufua katika wafu, nasi ndio mashahidi. Tena kwa hivyo, huyu alivyolitegemea Jina lake, hilo Jina lake limemtia nguvu huyu, mnayemwona na kumjua. Kweli hivyo, alivyolitegemea kwa kutiwa nguvu nalo, ndivyo vilivyompa huu uzima wote, mnaouona ninyi nyote.* Sasa, ndugu zangu, ninajua, ya kuwa mliyafanya pasipo kujua maana, kama wakubwa wenu nao. Lakini hivyo ndivyo, Mungu alivyoyatimiza, aliyoyatangaza kale kwa vinywa vya wafumbuaji wote kwamba: Kristo wake atateswa. Kwa hiyo juteni na kugeuka, makosa yenu yafutwe, yawatoke! Ndipo, zitakapowafikia nazo siku za kupoea usoni pa Bwana, tena ndipo, atakapopata kumtuma Kristo Yesu, mliyepewa kwanza. Ndiye, aliyempasa kuutwaa ufalme wa mbingu, mpaka siku zifike, vitu vyote vitakaporudishiwa upya, kama Mungu alivyosema hata kale kwa vinywa vya wafumbuaji wake watakatifu. Mose alisema: Miongoni mwa ndugu zenu Bwana Mungu atawainulia mfumbuaji atakayelingana na mimi, nanyi sharti mmsikie yote, atakayowaambia! Lakini itakuwa, kila mtu atakayekataa kumsikia yule mfumbuaji ataangamizwa, atengwe kabisa nao watu wa kwetu. Nao wafumbuaji wote toka kwa Samueli na wale waliofuata, wo wote waliosema, wamepiga mbiu za siku hizo. Ninyi m wana wao wafumbuaji, tena m wana wa Agano, Mungu aliloliagana na baba zenu alipomwambia Aburahamu: Katika uzao wako ndimo, mataifa yote ya nchi yatakamobarikiwa. Ninyi m wa kwanza, Mungu aliowafufulia mtoto wake na kumtuma, awabariki, mgeuke kila mmoja mkiyaepuka mabaya yenu. *Walipokuwa wakisema na watu, wakawajia watambikaji na mlinda Patakatifu na Masadukeo. Kwani walikasirika, kwa sababu walifundisha watu na kuwapigia mbiu ya kwamba: Wafu watafufuka kwa hivyo, Yesu alivyofufuka. Kwa hiyo wakawakamata, wakawatia kifungoni, mpaka asubuhi yake, kwani ilikuwa jioni. Lakini waliolisikia lile neno wengi wakalitegemea, waume tu wakawa kama 5000. Kulipokucha, wakakusanyika Yerusalemu wakubwa wao na wazee na waandishi na mtambikaji mkuu Ana na Kayafa na Yohana na Alekisandro nao wote waliokuwa wa ukoo wa mtambikaji mkuu. Kisha wakawasimamisha katikati, wakawauliza: Hilo ninyi mmelifanya kwa nguvu ya nani au kwa jina la nani? Ndipo, Petero alipojaa Roho takatifu, akawaambia: Nyie wakubwa wa watu wa kwetu na wazee, kwa kuwa mtu mwenye kilema amefanyiziwa vizuri, sisi twaulizwaulizwa leo: Huyu amepona kwa nguvu ya nani? Tambueni ninyi nyote na ukoo wote wa Isiraeli: Nguvu ya Jina la Yesu Kristo wa Nasareti, mliyemwamba msalabani ninyi, Mungu aliyemfufua katika wafu, hiyo nguvu yake ndiyo inayomsimamisha huyu mtu machoni penu, yuko mzima! Huyu ndiye lile jiwe lililokataliwa na ninyi waashi, lakini limekuwa jiwe la pembeni. Tena hapana pengine panapopatikana wokovu, wala hapana Jina jingine chini ya mbingu, sisi watu tulilopewa, tuokoke nalo.* Walipomwona Petero na Yohana, walivyosema pasipo woga, tena ilipowaelea, ya kuwa ni watu wasiofundishwa wala Maandiko wala ujuzi wo wote, wakastaajabu, wakawatambua, ya kuwa walikuwa pamoja na Yesu. Lakini walipomtazama yule mtu aliyeponywa, anavyosimama pamoja nao, hawakuwa na neno la kujibu. Wakawaagiza, watoke barazani kwao wakuu kwenda nje, wakala njama wao kwa wao wakisema: Tuwafanyieje watu hawa? Kwani wamefanya kielekezo cha waziwazi kinachotambulikana kwa watu wote wakaao Yerusalemu; nasi hatuwezi kukikana. Lakini kusudi isipate kuenea po pote kwa watu, tuwatishe, wasimwambie tena mtu ye yote jambo lo lote la Jina hilo. Kisha wakawaita, wakawakemea kabisa, wasiseme tena na kufundisha mambo ya Jina la Yesu. Lakini Petero na Yohana wakajibu wakiwaambia: Likateni shauri hilo wenyewe, kama inaongoka mbele ya Mungu, kuwasikia ninyi kuliko Mungu! Kwani sisi hatuwezi kuacha, tusiyaseme, tuliyoyaona nayo tuliyoyasikia. Lakini wakawatisha sana, wakawafungua, kwa sababu hawakuwaonea neno la kuwaumiza, kwa kuwa waliwaogopa watu. Kwani wote walimtukuza Mungu kwa yale yaliyofanyika, kwani yule mtu aliyefanyiwa kielekezo hivyo cha kuponywa, miaka yake ilipita 40. Walipokwisha funguliwa wakaenda kwa watu wao, wakawasimulia yote, watambikaji wakuu na wazee waliyowaambia. Walipoyasikia, ndipo, wote pamoja walipompalizia Mungu sauti na kusema: Bwana, wewe ndiwe uliyezifanya mbingu na nchi na bahari navyo vyote vilivyomo! Uliisemesha Roho takatifu kwa kinywa cha mtoto wako Dawidi: Mbona wamizimu hupiga makelele? Mbona makabila ya watu huwaza mambo yaliyo ya bure? Wafalme wa nchi hushikana mioyo? wakuu nao hula njama wakikaa pamoja, wamkatae Bwana na Kristo wake. Hii ni kweli, kwani walikusanyika mjini humu, wamkamate mtoto wako mtakatifu Yesu, uliyempaka mafuta; akina Herode na Pontio Pilato walipatana na wamizimu na watu wa Isiraeli, wayafanye yote, uliyomtakia kale kwa mkono wako na kwa mapenzi yako, kwamba yatimie papo hapo. Na sasa, Bwana, yatazame matisho yao! Wape watumwa wako waliseme Neno lako waziwazi pasipo woga hata kidogo! Unyoshe mkono, uponye watu na kufanya vielekezo na vioja kwa Jina la mtoto wako mtakatifu Yesu! Walipoomba hivyo, hapo, walipokuwa wamekusanyika, pakatetemeka, wakajazwa wote Roho Mtakatifu, wakalisema Neno la Mungu waziwazi pasipo woga. *Nao wigi wa watu waliokuwa wamemtegemea Bwana, mioyo yao nazo roho zao zilikuwa moja; tena hakuwako hata mmoja aliyezitumia mali zake, kama ni zake mwenyewe, lakini vyote walivitumia bia. Nao mitume wakaushuhudia ufufuko wa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi, magawio makuu ya Mungu yakiwakalia wao wote. Kwa hiyo hakupatikana kwao aliyekosa vitu, alivyopaswa navyo. Kwani wote waliokuwa wenye mashamba au nyumba waliziuza, wakaziweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa, kama alivyokosa.* Kulikuwa na Mlawi aliyetoka Kipuro, jina lake Yosefu, aliyeitwa na mitume Barnaba, maana yake Mwana wa Tulizo, naye alikuwa na shamba, akaliuza, akazileta fedha, akaziweka miguuni pa mitume. Kulikuwa na mtu jina lake Anania, na mkewe Safira; huyu alipouza kiunga akaficha fungu la fedha, alizozipata, naye mkewe alivijua. Kisha akaleta fungu moja, akaliweka miguuni pa mitume. Lakini Petero akasema: Anania, mbona Satani ameenea moyoni mwako, ukamdanganya Roho Mtakatifu na kuficha fungu la fedha za kiunga? Hakikuwa mali yako, uliyoweza kukaa nayo? Hata kilipokwisha kuuzwa, je? Hukuweza kufanya, kama ulivyopenda? Mbona umelitia jambo hilo moyoni mwako? Hukudanganya watu, ila umemdanganya Mungu. Anania alipoyasikia maneno haya akaanguka chini, akakata roho. Ndipo, woga mwingi ulipowaingia wote walioyasikia. Kisha vijana wakainuka, wakamfunga nguo, wakampeleka nje, wakamzika. Zilipopita kama saa tatu, mkewe akaingia, asiyajue yaliyofanyika. Petero akamwuliza: Niambie: Fedha, mlizozipata kwa kukiuza kiunga, ndizo hizi? Naye aliposema: Ndio, ni zizi hizi, Petero akamwambia: Mbona ninyi mmepatana kumjaribu Roho wa Bwana? Tazama, miguu yao waliomzika mumeo iko nje mlangoni, watakupeleka wewe nawe! Papo hapo akaanguka chini miguuni pake, akakata roho. Wale vijana walipoingia na kumkuta, amekufa, wakampeleka nje, wakamzika hapo pa mumewe. Ndipo, woga mwingi ulipowaingia wateule wote nao wote walioyasikia haya. Vikafanyika vielekezo na vioja vingi kwa mikono ya mitume kwa watu wa kwao, wale wote wakiwa pamoja katika ukumbi wa Salomo, kwa sababu mioyo yao ilikuwa ilikuwa mmoja. Lakini wengine hakuna hata mmoja aliyejipa moyo na kugandamiana nao, maana watu waliwakuza. Nao waliomtegemea Bwana wakaongezeka sana, ni vikundi vizima vya wanaume na vya wanawake. Kwa hiyo watu wakawatoa hata wagonjwa, wakawaweka njiani, wakilala vitandani au majamvini, kwamba Petero akipita, kivuli chake tu kiwafikie mmojammoja. Wakakusanyika hata watu wengi wa vijiji vilivyouzunguka Yerusalemu, wakaleta wagonjwa nao wenye kupagawa na pepo wachafu, wakaponywa wote. Pakainuka mtambikaji mkuu nao wote waliokuwa naye, ndio wa chama kile cha Masadukeo; kwa kujaa wivu wakawakamata mitume, wakawafunga na kuwapeleka kifungoni. Lakini usiku malaika wa Bwana akaifungua milango ya kifungoni, akawatoa, akasema: Nendeni, msimame Patakatifu kuwaambia watu wa kwenu maneno yote ya uzima huo! Walipoyasikia haya wakapaingia Patakatifu, kulipokucha, wakafundisha. Lakini mtambikaji mkuu nao waliokuwa pamoja naye wakaja, wakawakusanya wenzao wakuu na wazee wote wa wana wa Isiraeli, wakatuma watu bomani, wawalete. Hao watumishi walipofika hawakuwaona kifungoni, wakarudi, wakaleta habari wakisema: Kifungo tumekikuta, kimefungwa vizuri na kukazwa sana, hata walinzi tuliwaona, wamesimama milangoni; lakini tulipofungua hatukuona mtu ndani. Mlinda Patakafitu nao watambikaji wakuu walipoyasikia maneno haya wakahangaika sana, wasijue, jambo hilo litakavyokuwa. Pakaja mtu, akawasimulia: Tazameni, watu hao, mliowatia kifungoni, wamo nyumbani mwa Patakatifu, wamesimama na kufundisha watu! Ndipo, mlinda Patakatifu alipokwenda na watumishi, akawaleta, lakini si kwa nguvu, kwani waliwaogopa watu, wasije, wakawapiga mawe. Walipowaleta, wakawasimamisha mbele yao wakuu. Mtambikaji mkuu akawauliza: Hatukuwakemea kwa nguvu ya kwamba: Msifundishe mambo ya Jina hilo? Lakini tazameni, mafundisho yenu mmeyaeneza Yerusalemu, tena mwataka kutusingizia damu ya mtu yule. Ndipo, Petero na mitume walipojibu wakisema: Sharti tumtii Mungu kuliko watu! Mungu wa baba zetu amemfufua Yesu, mliyemwua ninyi na kumtundika mtini; huyo ndiye, Mungu aliyempaza na kumketisha kuumeni kwake, awe kiongozi na mponya, ajutishe Waisiraeli, wapate kuondolewa makosa. Nasi ndio mashahidi wa mambo hayo pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu aliyewapa wale waliomtii. Walipoyasikia haya wakakereza meno, wakataka kuwaua. *Kisha pakainuka hapo penye wakuu Fariseo, jina lake Gamalieli; ni mfunzi wa Maonyo mwenye cheo kwa watu wote, akaagiza, wale watu wapelekwe nje kidogo. Kisha akawaambia: Waume Waisiraeli, jilindeni kwa ajili ya hayo, mtakayowatendea watu hawa! Kwani mbele ya siku hizi aliondokea Teuda, akajiwazia, kwamba yeye ndiye mtu, nao watu waliomfuata wakapata kama 400. Alipouawa, wote waliomtii wakatawanyika, wakapoteapotea, tena hakuna kitu. Kisha katika siku za kuandikiwa kodi aliondokea Yuda Mgalilea, akatenga kikundi cha watu, wamfuate yeye. Naye alipoangamia, wote waliomtii wakatawanyika nao. Kwa hiyo sasa nawaambiani: Mtengamane na watu hawa, mwaache! Kwani mawazo hayo au kazi hizo zikiwa zimetoka kwa watu zitakoma; lakini zikiwa zimetoka kwake Mungu, hamwezi kuwakomesha, msije mkaonekana, ya kuwa mnagombana na Mungu. Ndipo, walipomwitikia, wakawaita wale mitume, wakawapiga, wakawakemea, wasiseme tena mambo ya Jina la Yesu, kisha wakawafungua. Wao wakatoka machoni pa wakuu wakichangamka, kwa sababu Mungu amewapa kutwezwa kwa ajili ya Jina lake. Siku zote hawakuacha kufundisha na kuutangaza Utume mwema wa Yesu Kristo hapo Patakatifu na nyumbani mo mote.* Siku zile wanafunzi walipozidi kuwa wengi, Wagriki waliwanung'unikia Waebureo, kwani wanawake wajane wa kwao hawakutumikiwa kama wengine na kugawiwa kila siku vilivyowapasa. Hapo wale kumi na wawili wakawakusanya wingi wa wanafunzi, wakasema: Haifai, sisi tukiliacha Neno la Mungu, tutumikie mezani. Ndugu zetu, mkague watu saba wa kwenu wanaojulikana, ya kuwa wamejaa Roho na werevu wa kweli, tuwaweke, walitumikie jambo hilo! Lakini sisi tuishike kazi yetu ya kuomba na kulitumikia Neno. Neno hili likawapendeza wale wote waliokuwako, wakamchagua Stefano aliyekuwa mwenye kumtegemea Bwana kwa moyo wote na mwenye Roho takatifu na Filipo na Porokoro na Nikanoro na Timoni na Parmena na Nikolao aliyekuwa mfuasi wa Kiyuda wa Antiokia. Hawa ndio, waliowasimamisha mbele ya mitume, wakawabandikia mikono wakiwaombea kwa Mungu. Hivyo Neno la Mungu likaendelea, wanafunzi wakapata kuwa wengi sana Yerusalemu, hata watambikaji wengi wakamtegemea Bwana na kumtii. Naye Stefano alikuwa mwenye nguvu nyingi za kumtegemea Bwana, akafanya vioja na vielekezo vikubwa mbele ya watu. Kwa hiyo wakainuka wengine waliokuwa wa chama kilichoitwa cha Walibertino na watu wa Kirene na wa Alekisandria nao walitoka Kilikia na Asia, wakaulizana na Stefano. Lakini hawakuweza kuyabisha, aliyoyasema kwa werevu uliokuwa wa kweli na kwa Roho. Ndipo, walipoleta watu wengine waliosema: Tumemsikia, alivyosema maneno ya kumbeza Mose na Mungu. Wakawachafua watu na wazee na waandishi, wakamjia, wakamkamata, wakampeleka barazani kwa wakuu. Wakasimamisha mashahidi wa uwongo waliosema: Mtu huyu haachi kusema maneno ya kupakataa mahali Patakatifu, hata maonyo. Kwani tumesikia, alivyosema: Yesu wa Nasareti atapabomoa mahali hapa na kuzigeuza desturi, Mose alizotupa. Ndipo, wote waliokaa barazani kwa wakuu walipomkazia macho, wakauona uso wake kuwa kama uso wa malaika. Mtambikaji mkuu alipomwuliza: Ndivyo, yalivyo mambo haya? akasema: Waume ndugu na baba, sikilizeni! Mungu mwenye utukufu alimtokea baba yetu Aburahamu, alipokaa Mesopotamia, alipokuwa hajahamia Harani, akamwambia: Toka katika nchi yako kwenye ndugu zako, uende katika nchi, nitakayokuonyesha! Ndipo, alipotoka katika nchi ya Wakasidi, akahamia Harani. Tena, baba yake alipokwisha kufa, akamhamisha toka huko, akamweka katika nchi hii, mnayoikaa ninyi sasa. Lakini hakumpa fungu humu, ingawa liwe limelingana na wayo; ila alipokuwa hana mtoto, aliagana naye, ya kuwa atampa, aitwae nchi hii yeye nao wa uzao wake wajao nyuma yake. Kisha Mungu akavisema: Wao wa uzao wake watakaa ugenini katika nchi ngeni, wale wawafanyishe kazi za watumwa na kuwasumbua vibaya miaka 400. Nalo taifa lile, ambalo watalifanyika kazi za watumwa, nitawahukumu mimi, wale wapate kuhama huko, wanitumikie mahali hapa; ndivyo, alivyosema Mungu. Kisha akampa agano la tohara; kwa hiyo alipomzaa Isaka akamtahiri siku ya nane; naye Isaka akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa babu zetu wakuu kumi na wawili. Wale babu zetu wakuu wakamwonea Yosefu wivu, wakamwuza kwenda Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, akamwokoa katika maumivu yake yote, akamgawia kipaji cha werevu wa kweli, apate kusema mbele ya Farao, mfalme wa Misri; ndiye aliyemweka kuwa mkubwa, aitawale Misri na nyumba yake yote. Njaa ilipokuja kuiingia Misri yote na Kanaani, yakawa maumivu makubwa, baba zetu nao wasione vya kujishibisha. Lakini Yakobo aliposikia, ya kuwa Misri ziko ngano, akawatuma baba zetu mara ya kwanza. Katika safari ya pili Yosefu akajitambilisha kwa ndugu zake, nako kwa Farao ukoo wa Yosefu ukajulika. Kisha Yosefu akatuma watu, akamwita baba yake Yakobo na ndugu zake wote, wakawa kama 75. Ndipo, Yakobo alipotelemka kwenda Misri. Huko akafa yeye mwenyewe nao baba zetu, wakapelekwa Sikemu, wakazikwa katika kaburi, alilolinunua Aburahamu na fedha kwa wana wa Hamori kule Sikemu. Siku zilipokaribia, Mungu alizoziagana na Aburahamu na kujiapisha, watu wa kwetu wakazidi kuwa wengi sana huko Misri, mpaka alipoondokea mfalme mwingine wa Misri asiyemjua Yosefu. Huyo akawaendea wao wa kizazi chetu kwa udanganyi, akawatendea baba zetu maovu akiagiza, vitoto vyao vichanga watupwe, wasikae kuwa wazima. Siku zile Mose akazaliwa, Mungu akapendezwa naye. Kwa hiyo akalelewa miezi mitatu nyumbani mwa baba yake; kisha alipotupwa, binti Farao akamwokota, akamlea, awe mwanawe yeye. Naye Mose akafundishwa ujuzi wote wa Wamisri, akawa mwenye nguvu kwa maneno na kwa matendo yake. Tena miaka yake ilipopata 40, moyo wake ukamtuma kuwakagua ndugu zake, wale wana wa Isiraeli. Alipoona, mmoja anavyoumizwa bure tu, akamsaidia yule aliyepigwa, akamlipiza yule Mmisri akimwua. Akadhani, ndugu zake watajua, ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake yeye; lakini hawakujua. Kulipokucha, akawajia tena, akawaona, wakipigana; akawaamua, wapatane, akisema: Waume, ninyi m ndugu, mbona mnakorofishana? Lakini yule aliyemkorofisha mwenziwe akamsukuma akisema: Yuko nani aliyekuweka kuwa mkuu mwamuzi kwetu? Je? Wewe unataka kuniua nami, kama ulivyomwua jana yule Mmisri? Kwa ajili ya neno hilo Mose akakimbia, akawa mgeni katika nchi ya Midiani. Ndiko, alikozaa wana wawili. Ilipokwisha pita tena miaka 40, malaika akamtokea porini mlimani kwa Sinai katika kichaka kilichowaka moto. Mose alipoyaona hayo akastaajabu; lakini alipopakaribia kuyatazama akasikia, Bwana akisema: Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Aburahamu na wa Isaka na wa Yakobo. Ndipo, Mose alipotetemeka, hakupata moyo wa kupatazama. Naye Bwana akamwambia: Vivue viatu miguuni pako! Kwani hapa, unaposimama, ni nchi takatifu. Nimeyaona mateso yao walio ukoo wangu walioko Misri; nikasikia, wanavyopiga kite, nikashuka, niwaokoe. Sasa njoo! Nitakutuma, uende Misri. Huyo Mose, waliomkataa na kusema: Yuko nani aliyekuweka kuwa mkubwa na mwamuzi? huyo ndiye, Mungu aliyemtuma kuwa mkubwa na mwokozi, awaokoe kwa mkono wa malaika aliyemtokea kichakani. Kisha huyo akawatoa na kufanya vioja na vielekezo katika nchi ya Misri na katika Bahari Nyekundu, kisha nako jangwani miaka 40. Huyo ndiye yule Mose aliyewaambia wana wa isiraeli: Miongoni mwa ndugu zenu Mungu atawainulia mfumbuaji atakayelingana na mimi. huyo ndiye aliyekuwa penye wateule jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye mlimani kwa Sinai, tena pamoja na baba zetu. Ndiye aliyepokea maneno ya uzima, atupe sisi; tena ndiye, ambaye baba zetu hawakutaka kumtii, wakamsukuma, wakageuka mioyoni mwao, kwamba warudi Misri, wakamwambia Haroni: Tufanyie miungu itakayotuongoza! Kwani huyo Mose aliyetutoa katika nchi ya Misri hatuyajui yaliyompata. Siku zile wakatengeneza ndama, nacho kinyago hicho wakakitolea ng'ombe za tambiko, nacho kilichokuwa kazi ya mikono yao wakakishangilia. Kisha Mungu akageuka, akawatupa, wavitumikie vikosi vya mbinguni, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Wafumbuaji: Je? Ng'ombe na vipaji, mlivyovitoa nyikani miaka 40, vilikuwa vya kunitambikia mimi, ninyi mlio mlango wa Isiraeli? Hapana, ila mlikuwa mmejitwika hema la Moloko na nyota za mungu wa Romfa; hivyo vinyago, mlivyovitengeneza, ndivyo, mlivyovitumia vya kuviangukia. Kwa hiyo nitawahamisha ninyi, mwende mbali kupita Babeli. Baba zetu walipokuwa jangwani walikuwa nalo lile Hema la Ushahidi, kama mwenye kusema na Mose alivyoagiza na kumwambia, alitengeneze kwa mfano, aliouona. Nao baba zetu wakalipokea tena wakiongozwa na Yosua, wakaliingiza katika nchi ya wamizimu, Mungu aliowafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Dawidi. Huyo akaonea mapendeleo machoni pa Mungu, akaomba ruhusa ya kumpatia Mungu wa Yakobo makazi, lakini Salomo ndiye aliyemjengea Nyumba. Lakini yeye Alioko huko juu hakai katika nyumba zilizojengwa na mikono ya watu. Ndivyo, anavyosema mfumbuaji: Mbingu ni kiti changu cha kifalme, nayo nchi ni pa kuiwekea miguu yangu. kwa hiyo Bwana anasema: Ni nyumba gani, mtakayonijengea? Au mahali pa kupumzikia mimi ni mahali gani? Sio mkono wangu ulioyafanya hayo yote? Ninyi wenye kosi ngumu, ninyi wenye mioyo na masikio yaliyo kama ya watu wasiotahiriwa, ninyi kila mara humpinga Roho Mtakatifu, kama walivyofanya baba zenu, vivi hivi ninyi nanyi. Ni mfumbuaji gani, ambaye baba zenu hawakumfukuza? Nao walianza kupiga mbiu za kuja kwake huyo Mwongofu waliwaua, tena ni yuleyule, mliyemchongea, kisha mkamwua; Maonyo mliyapokea kwa kuagizwa na malaika, lakini hamkuyalinda. Walipoyasikia haya wakachomwa mioyoni mwao, wakamkerezea meno. Lakini yeye akajaa Roho takatifu, akayaelekeza macho mbinguni akaona utukufu wa Mungu, akamwona naye Yesu, akiwa amesimama kuumeni kwa Mungu, akasema: Tazameni, naziona mbingu, zimefunuka, naye Mwana wa mtu amesimama kuumeni kwa Mungu. Ndipo, walipopiga kelele na kupaza sauti na kujiziba masikio, wakamrukia wote pamoja, wakamkumba, atoke mjini, wakampiga mawe. Kulikuwako mashahidi, nao wakazivua nguo zao, wakaziweka miguuni pa kijana, jina lake Sauli, kisha nao wakampiga Stefano mawe, yeye akiomba na kusema: Bwana Yesu, ipokee roho yangu! Kisha akapiga magoti, akaita kwa sauti kuu: Bwana, usiwawekee kosa hili! Alipokwisha kuyasema haya akalala. Sauli naye alikuwa amependezwa na kuuawa kwake. Siku ile wateule waliokuwamo Yerusalemu wakashambuliwa na kufukuzwa kabisa; kwa hiyo wote wakatawanyika katika nchi za Yudea na za Samaria; waliosalia ni mitume tu. Ndipo, watu wengine wenye kumcha Mungu walipomzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Lakini Sauli akawajengua wateule, akaingia nyumba kwa nyumba, akawakokota waume na wanawake, akawatia kifungoni. Wale waliotawanyika wakapita huko na huko wakiipiga mbiu njema ya lile Neno. Filipo akashuka kuuingia mji wa Samaria, akawapigia mbiu ya Kristo; watu wengi wakashikamana na yale yaliyosemwa na Filipo, mioyo yao ikawa mmoja tu kwa hayo, waliyoyasikia na kuviona vielekezo, alivyovifanya. Kwani wengi waliopagawa na pepo wachafu walitokwa nao, wakipiga makelele makubwa, hata wengi waliokuwa wenye kupooza na viwete wakapona. Mjini mle mkawa na furaha nyingi. Kulikuwa na mtu mjini mle, jina lake Simoni, aliyekuwa akiwahangaisha watu wote wa Samaria kwa uganga wake akijisemea mwenyewe: Mimi ni mwenye uwezo. Wote, wadogo hata wakubwa, wakashikamana naye wakisema: Huyu ndio uwezo wa Mungu unaoitwa mkuu. Lakini walishikamana naye, kwa sababu aliwahangaisha siku nyingi kwa uganga wake. Lakini walipomtegemea Filipo aliyewapigia mbiu njema ya ufalme wa Mungu na ya Jina la Yesu Kristo, wakabatizwa, waume na wake. Hata Simoni mwenyewe akamtegemea Mungu, akabatizwa, akashikamana na Filipo; alipoona vielekezo na matendo makuu ya nguvu yaliyofanyizwa naye akahangaika moyoni. Mitume waliokuwa Yerusalemu waliposikia, ya kuwa Wasamaria wamelipokea Neno la Mungu, wakamtuma Petero na Yohana, waende kwao. Nao wakashuka, wakawaombea, wapewe Roho takatifu. Kwani kwao hakuna hata mmoja aliyeshukiwa nayo, walikuwa wamebatiziwa tu Jina la Bwana Yesu. Papo hapo, wale walipowabandikia mikono, walipewa Roho takatifu. Lakini Simoni alipoona, ya kuwa watu hupewa Roho, mitume wakiwabandikia mikono, akawaletea fedha, akasema: Nipeni nami nguvu hii, mtu nitakayembandikia mikono apewe Roho takatifu! Lakini Petero akamwambia: Fedha zako na ziangamie pamoja na wewe, kwa sababu umewaza, ya kuwa gawio lake Mungu linanunulika kwa mali! Wewe jambo hili hugawiwi hata kifungu tu, kwani moyo wako haukunyoka mbele ya Mungu. Sharti ujute na kuuacha huu uovu wako, ukimwomba Bwana, labda utapata kuondolewa mawazo ya moyo wako. Kwani nakuona, unayo yaliyo machungu kama nyongo, tena u mtumwa wa upotovu. Ndipo, Simoni alipojibu akisema: Niombeeni ninyi kwa Bwana mambo hayo, mliyoyasema, yasinipate hata moja! Walipokwisha kulishuhudia Neno la Bwana na kulisema po pote wakarudi kwenda Yerusalemu wakiipiga hiyo mbiu njema katika vijiji vingi vya Wasamaria. *Malaika wa Bwana akamwambia Filipo akisema: Inuka, uende upande wa kusini, uifuate barabara itelemkayo toka Yerusalemu kwenda Gaza, ileile iliyokwisha kufa. Ndipo, alipoinuka akaenda. Mara akaona mtu wa Etiopia; huyu alikuwa mtunza mali na mtu mwenye nguvu wa Kandake, mfalme wa kike wa Etiopia, alizisimamia mali zake zote. Alikuwa amekwenda Yerusalemu kula sikukuu. Lakini alipokuwa anarudi na kukaa garini mwake alikisoma kitabu cha mfumbuaji Yesaya. Ndipo, Roho alipomwambia Filipo: Haya! Lijongelee gari hili, ulifuatefuate! Filipo akamwendea mbio, akamsikia, alivyokisoma kitabu cha mfumbuaji Yesaya; alipomwuliza: Unayatambua, unayoyasoma? akasema: Nitawezaje, mtu asiponiongoza? akambembeleza Filipo, apande, akae pamoja naye. Nalo fungu la Maandiko, alilolisoma, lilikuwa hili: Kama kondoo alipelekwa kuchinjwa; kama mwana kondoo anavyomnyamazia mwenye kumkata manyoya, vivyo hivyo naye hakukifumbua kinywa chake. Kwa hivyo, alivyonyenyekea, alinyimwa uamuzi mnyofu; yuko nani atakayesimulia, ukoo wake ulivyokuwa? Kwani ameondolewa katika nchi yao walio hai, asikae nchini. Mtunza mali akamwuliza Filipo akisema: Nakuomba, uniambie: Haya mfumbuaji anayasema ya nani? Anajisema mwenyewe au anamsema mwingine? Ndipo, Filipo alipokifumbua kinywa chake, akaanza kwa Maandiko yale yale akimpigia mbiu ya Yesu. Walipoendelea njiani wakafika penye maji kidogo, mtunza mali akasema: Tazama, yako maji, iko nini tena inayozuia, nisibatizwe? Filipo akasema: Ukimtegemea Bwana kwa moyo wako wote, inawezekana. Ndipo, alipojibu akisema: Namtegemea Yesu Kristo kuwa Mwana wake Mungu; kisha akaagiza, gari lisimame, wakashuka wote wawili majini, Filipo na mtunza mali, akambatiza.* Lakini walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana alimpokonya Filipo, mtunza mali asimwone tena. Kisha akaishika njia yake na kufurahi. Lakini Filipo akaonekana Asdodi akiipiga hiyo mbiu njema katika miji yote, aliyoipita, hata akafika Kesaria. Naye Sauli alikuwa akingali bado akiwatolea wanafunzi wa Bwana ukorofi kwa kuwatisha na kwa kuwaua. Akamwendea mtambikaji mkuu, akataka kwake barua za kwenda Damasko, aende nazo kwenye nyumba za kuombea za Wayuda, kwa maana alitaka kuwafunga na kuwapeleka Yerusalemu wo wote, atakaowaona wa njia hiyo, wakiwa waume au wake. Lakini alipokuwa akienda na kufika karibu ya Damasko, mara akamulikiwa na mwanga uliotoka mbinguni, akaanguka chini, akasikia sauti iliyomwambia: Sauli, Sauli, unanifukuzaje? Alipouliza: Ndiwe nani, Bwana? akajibu: Mimi ni Yesu, ambaye unanifukuza wewe. Utashindwa na kupiga mateke penye machomeo. Lakini inuka, uingie mjini! Ndimo, utakamoambiwa yakupasayo, uyafanye. Lakini wenziwe waliokuwa pamoja naye njiani walikuwa wamesimama, wasiweze kusema, kwa sababu waliusikia uvumi, wasione mtu. Sauli alipoinuka chini, macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; kwa hiyo wakamshika mkono, wakampeleka Damasko. Siku tatu akawapo, asione kitu, wala asile, wala asinywe. Mlikuwa na mwanafunzi mle Damasko, jina lake Anania. Huyo Bwana akamwambia katika njozi: Anania! Aliposema: Tazama, nipo hapa Bwana! Bwana akamwambia: Inuka, uende kufika penye barabara inayoitwa Nyofu, uulize nyumbani mwa Yuda, kama yumo mtu wa Tarso, jina lake Sauli. Kwani tazama, yumo katika kuomba. Naye ameona mtu, jina lake Anania, anavyoingia humo, alimo, ambandikie mikono, apate kuona tena. Anania akajibu: Bwana, nimesikia kwa watu wengi maovu yote, mtu huyo aliyowafanyia watakatifu wako walioko Yerusalemu. Tena amepata ruhusa kwa watambikaji wakuu kuwafunga hapa wote pia wanaolitambikia Jina lako. Lakini Bwana akamwambia: Nenda tu! Kwani mtu huyu ataniwia chombo kiteule cha kulipeleka Jina langu mbele yao wamizimu na wafalme na wana wa Isiraeli. Nami nitamwonyesha mateso yote, atakayoteswa kwa ajili ya Jina langu. Kisha Anania akaondoka, akaenda, akaingia nyumbani mle, akambandikia mikono akisema: Ndugu yangu Sauli, Bwana Yesu aliyekuotokea njiani, alipokuja, amenituma, upate kuona tena na kujazwa Roho takatifu. Papo hapo pakawa kama magamba yaliyoanguka toka machoni pake, akaona, tena akainuka, akabatizwa. Naye alipokwisha kula chakula akapata nguvu tena. Akakaa siku kidogo, pamoja na wanafunzi waliokuwamo Damasko, hakukawia kuipiga mbiu ya Yesu katika nyumba za kuombea akisema: Huyo ndiye Mwana wa Mungu. Wote waliomsikia wakahangaika mioyoni, wakasema: Je? Huyu siye aliyekuwa akiwateka Yerusalemu waliolitambikia Jina hili? Huku nako hakuyajia yayo hayo kuwafunga na kuwapeleka kwa watambikaji wakuu? Lakini Sauli akakaza kutenda nguvu, akawatatanisha Wayuda waliokaa Damasko akiwashinda kwa kusema: Huyu ndiye Kristo. Siku zilipokwisha pita nyingi, Wayuda wakala njama ya kumwangamiza, lakini Sauli alipata kuitambua njama yao. Walipomwotea malangoni pa mji mchana na usiku, wapate kumwangamiza, ndipo, wanafuanzi walipomchukua usiku, wakamtia kapuni, wakamshusha ukutani. Alipofika Yerusalemu akajaribu kugandamiana na wanafunzi, wote wakiwa wakingali na woga wa kumwogopa, wasiitikie, ya kuwa ni mwanafunzi; ndipo, Barnaba alipomchukua, akampeleka kwa mitume, akawasimulia, alivyomwona Bwana njiani, navyo alivyosema naye, tena alivyolitangaza Jina la Yesu huko Damasko waziwazi. Kisha akafuatana nao akiingia, tena akitoka nao Yerusalemu, akalitangaza Jina la Bwana waziwazi. Hata Wayuda waliotoka Ugriki akasema nao na kubishana nao. Ndipo, walipotafuta njia ya kumwangamiza. Lakini ndugu walipoyatambua wakamsindikiza mpaka Kesaria, wakamtuma kwenda zake Tarso. Hivyo wateule walitengamana pote katika Yudea na Galilea na Samaria, wakajijenga, wakaendeleana kwa kumcha Bwana, tena wakawa wengi wakitulizwa na Roho Mtakatifu. Ikawa, Petero alipopita pote akashuka na kuwafikia hata watakatifu waliokaa Lida. Huko akaona mtu, jina lake Enea, alikuwa amepooza na kulala kitandani miaka minane. Petero akamwambia: Enea, Yesu Kristo anakuponya; inuka, ujitandikie mwenyewe! Papo hapo akainuka. Walipomwona wao wote waliokaa Lida na Saroni, wakageuka, wamfuate Bwana. Yope mlikuwamo mwanafunzi mwanamke, jina lake Tabea, maana yake ni Paa. Huyu alikuwa na matendo mema mengi ya kugawia wengi. Ikawa, siku zile akaugua, akafa; kisha wakamwosha, wakamlaza katika chumba cha juu. Kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu ya Yope, wanafunzi walisikia, ya kuwa Petero yuko huko; kwa hiyo wakatuma kwake watu wawili, wamwombe, asikawie kuja kwao. Petero akainuka, akaenda nao. Alipofika, wakapanda naye kwenda katika chumba cha juu. Humo wanawake wajane wote wakamjia, wakasimama wakilia na kumwonyesha kanzu na nguo zote, alizowashonea yule Paa alipokuwa pamoja nao. Petero akawatoa wote, waje nje, akapiga magoti, akamwomba Mungu na kuugeukia ule mwili wake, akasema: Tabea, inuka! Ndipo, alipoyafumbua macho yake; alipomwona Petero akajiketisha. Naye akamshika mkono, akamwinua, akawaita wale watakatifu na wale wajane, akamsimamisha mbele yao, akiwa yu hai. Vikaja kutambulikana Yope mjini mote; kwa hiyo wengi wakamtegemea Bwana. Akakaa siku nyingi huko Yope kwa fundi wa kutengeneza ngozi, jina lake Simoni. Kesaria kulikuwa na mtu, jina lake Kornelio, mkubwa wa kikosi cha askari kilichoitwa cha Italia. Naye alimtii Mungu na kumcha pamoja nao wote wa nyumbani mwake: wengi wa kwao aliwagawia vipaji vingi, tena alikuwa akimwomba Mungu po pote. Siku moja, alipokuwa kama saa tisa ya mchana, akaona njozi, yuko macho, akaona, malaika wa Mungu akiingia nyumbani mwake na kumwambia: Kornelio! Naye akamkazia macho, akashikwa na woga, akasema: Nini, Bwana? Akamwambia: Maombo yako na magawio yako yamefika juu machoni pa Mungu, anayakumbuka. Sasa hivi tuma watu, waende Yope, wamlete Simoni anayeitwa Petero! amefikia kwa mtengenezaji wa ngozi, jina lake Simoni, nyumba yake iko pwani. Malaika aliyesema naye alipokwenda zake, akaita watumishi wawili na askari mwenye kumcha Mungu miongoni mwao walioshikana naye siku zote, akawasimulia yote, akawatuma, waende Yope. Kesho yake wale walipokuwa njiani na kuufikia mji karibu, Petero alikuwa amepanda kwenda katika chumba cha juu, aombe, saa sita ilipofika. Akaumwa na njaa, akataka kula. Walipomwandalia, akaingiwa na kituko, kwani anaona: mbingu imefunuka, kutoka mle panashuka chombo kinachofanana na guo kubwa, linatelemshwa chini, likishikwa kwa pembe zake nne. Mle ndani wamo nyama wote wenye miguu minne nao watambaao chini nao ndege wa angani. Kisha akasikia sauti ya kumwambia: Inuka, Petero, uchinje, ule! Ndipo, Petero aliposema: Hapana, Bwana! Kwani zamani zote sijala bado kilicho chenye mwiko au kisichotakata. Lakini sauti ikamwambia mara ya pili: Mungu alivyovitakasa, wewe usivizie! Vikafanyika hivyo mara tatu; kisha chombo kikapazwa mbinguni papo hapo. Petero alipopotelewa moyoni mwake, asijue maana ya hayo, aliyoyaona, papo hapo wale watu waliotumwa na Kornelio wakasimama mlangoni wakiiuliza nyumba ya Simoni. Wakapaza sauti na kuuliza, kama ndimo, Simoni anayeitwa Petero alimofikia. Naye Petero alipoyafikiri moyoni, aliyoyaona, Roho akamwambia: Tazama, pana watu watatu wanaokutafuta! Lakini inuka, ushuke, ufuatane nao pasipo mashaka! Kwani aliyewatuma ni mimi. Ndipo, Petero aliposhuka, akawajia wale watu, akawaambia: Tazameni, mnayemtafuta ni mimi. Mmekuja kwa sababu gani? Nao wakasema: Kornelio aliye mkubwa wa askari ni mtu mwongofu, mwenye kumcha Mungu, hata wote wa taifa la Wayuda wanamsemea vizuri; huyo ameagizwa na malaika mtakatifu, atume kwako, uje nyumbani mwake, ayasikie, utakayomwambia. Ndipo, alipowakaribisha na kuwafikiza. Kesho yake akainuka, akatoka pamoja nao, hata wengine wa Yope waliokuwa ndugu wakaenda pamoja naye. Siku ya kesho akaingia Kesaria. Naye Kornelio alikuwa akiwangoja; kwa hiyo alikuwa amewakusanya ndugu zake nao walio wapenzi wake wa kweli. Petero alipoingia, Kornelio akamwendea, akamwamkia na kumwangukia miguuni. Lakini Petero akamwinua akisema: Simama! kwani mimi nami ni mtu tu. Akaongea naye akiingia ndani; akawakuta wengi waliokusanyika, akawaambia: Ninyi mmejua, ya kuwa mtu wa Kiyuda ana mwiko wa kugandamiana na mtu wa kabila jingine au kumfikia. Lakini Mungu amenionyesha, nisimwazie mtu wo wote, kwamba ni wa mwiko au wa mzio. Kwa sababu hiyo nimekuja pasipo kubisha, ulipotuma kwangu. Sasa nawauliza: Ni neno gani, mlilonitumia? Kornelio akasema: Leo ni siku ya nne, tangu nilipokuwa nikifunga mpaka saa hii, tena nikimwomba Mungu nyumbani mwangu, saa tisa ilipofika. Papo hapo mtu alisimama mbele yangu aliyevaa nguo zilizomerimeta. Naye akasema: Kornelio, maombo yako yamesikiwa, nayo magawio yako yamekumbukwa mbele ya Mungu. Tume watu, waende Yope, wamwite Simoni anayeitwa Petero! Huyu amefikia nyumbani mwa Simoni aliye mtengenezaji wa ngozi, anakaa pwani. Papo hapo nikatuma kwako, nawe umefanya vema ukija. Sasa sisi sote tupo hapa mbele ya Mungu, tuyasikilize yote, uliyoagizwa na Bwana. *Petero akakifumbua kinywa chake, akasema: Naitambua kabisa iliyo kweli, ya kuwa Mungu hautazami uso wa mtu, lakini katika mataifa yote anayemcha yeye na kufanya yaongokayo humpendeza. Neno lake alilituma, liwafikie wana wa Isiraeli, akiwapigia ile mbiu njema ya utengemano uliopatikana kwa Yesu Kristo. Huyu ndiye Bwana wao wote. Ninyi mnayajua mambo yale yaliyofanyika katika nchi yote ya Yudea, yaliyoanza huko Galilea, Yohana alipokwisha kuutangaza ubatizo wake. Yesu wa Nasareti, Mungu alipomchagua kuwa mfalme na kumpa Roho takatifu na uwezo, alipita huko na huko akifanya mema na kuwaponya wote waliopagawa na yule Msengenyaji, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye. Nasi tumeyaona yote, aliyoyafanyiza katika nchi ya Wayuda namo Yerusalemu. Huyo walimwangamiza na kumtundika mtini, lakini Mungu akamfufua siku ya tatu, akamtuma, atokee; lakini sio watu wote waliotokewa naye, ni sisi tu tuliochaguliwa na Mungu kale, tuwe mashahidi; ni sisi tuliokula, tena tuliokunywa pamoja naye, alipokwisha kufufuka katika wafu.* *Akatuagiza kutangazia watu na kuyashuhudia po pote, ya kuwa ndiye aliyewekwa na Mungu, awahukumu wanaoishi nao waliokufa. Kwa kumwelekea huyu Wafumbuaji wote hushuhudia, ya kuwa kila atakayemtegemea atapata kuondolewa makosa kwa Jina lake. Petero akingali akiyasema maneno haya, Roho Mtakatifu akawaguia wote waliolisikia lile neno. Ndipo, wenye kumtegemea Bwana waliotahiriwa, waliokuja pamoja na Petero, waliposhangaa sana, ya kuwa hata wamaizimu humiminiwa kipaji cha Roho Mtakatifu. Kwani waliwasikia, wakisema misemo migeni na kumkuza Mungu. Ndipo, Petero alipojibu: Yuko nani anayeweza kukataza maji, hawa wasibatizwe waliompokea Roho Mtakatifu sawasawa kama sisi? Akaagiza, wabatizwe katika Jina la Yesu Kristo.* Kisha wakamwomba, akae kwao siku kidogo. Mitume na ndugu waliokuwako Yudea wakasikia, ya kuwa hata wamizimu wamelipokea Neno la Mungu. Petero alipopanda kwenda Yerusalemu, waliotahiriwa wakabishana naye wakisema: Umeingia mwa watu wasiotahiriwa, ukala pamoja nao. Petero akaanza kuwaeleza yote, yalivyofuatana, akisema: Mimi nilipokuwa katika mji wa Yope nikimwomba Mungu, nikaingiwa na kituko kwa kuona njozi: chombo kinachofanana na guo kubwa linatelemshwa chini toka mbinguni likishikwa kwa pembe zake nne likaja mpaka hapo, nilipokuwa. Nami nilipochungulia mle nikitazama, nikaona, mna nyama wenye miguu minne wa nchini nao nyama wa mwituni nao watambao nao ndege wa angani; kisha nikasikia sauti ya kuniambia: Inuka, Petero, uchinje, ule! Ndipo, niliposema: Hapana, Bwana, kwani cho chote kilicho chenye mwiko au kisichotakata hakijaingia bado kinywani mwangu. Lakini sauti ikanijibu tena toka mbinguni: Mungu alivyovitakasa, wewe usivizie! Vikafanyika hivyo mara tatu, kisha yote yakavutwa tena na kupazwa mbinguni. Mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba, nilimokuwa, walitumwa kwangu toka Kesaria. Naye Roho akaniambia, niende pamoja nao pasipo mashaka; hata hawa ndugu sita wakafuatana nami, tukaingia nyumbani mwake yule mtu. Huyo akatusimulia, alivyoona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kusema: Tume watu, waende Yope, wamwite Simoni anayeitwa Petero! Ndiye atakayekuambia maneno yatakayokuokoa wewe nao wote wa nyumbani mwako. Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akawaguia, kama alivyotuguia hata sisi hapo kwanza. Ndipo, nilipolikumbuka neno la Bwana, alilolisema: Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatiza katika Roho takatifu. Mungu alipowapa kipaji kilekile, tulichokipata na sisi tuliomtegemea Bwana Yesu Kristo, hapo mimi nilikuwa na nguvu gani, niweza kumzuia Mungu? Walipoyasikia haya wakanyamaza kimya, wakamtukuza Mungu wakisema: Kumbe hata wamizimu Mungu amewapa majuto, nao wapate uzima! Wale waliotawanyika kwa sababu ya maumivu, waliyopatwa nayo, Stefano alipouawa, wakazunguka, wakafika mpaka Ufoniki na Kipuro na Antiokia, wasimwambie mtu hilo Neno pasipo Wayuda peke yao. Lakini wengine wao walikuwa watu wa Kipuro nao wa Kirene. Hao walipofika Antiokia, wakawapigia hata Wagriki mbiu njema ya Bwana Yesu. Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, wakawa wengi waliomgeukia Bwana kwa kumtegemea. Hilo neno lao liliposikilika masikioni pa wateule waliokuwa huko Yerusalemu, wakamtuma Barnaba, aende Antiokia. Naye alipofika na kuviona vipaji, Mungu alivyowagawia, akafurahi, akawahimiza wote, wakaze mioyo kushikamana na Bwana. Kwa kuwa mtu mwema aliyejaa Roho takatifu alizidi kumtegemea Mungu; kwa hiyo kikundi kizima cha watu kikapelekwa kwa Bwana. Kisha akatoka kwenda Tarso kumtafuta Sauli; alipomwona akampeleka Antiokia. Kisha wakakaa nao wateule wa hapo hata mwaka mzima, wakafundisha watu wengi; napo hapo Antiokia ndipo, wanafunzi walipoanza kuitwa Wakristo. Ikawa siku zile, wakashuka wafumbuaji toka Yerusalemu kufika Antiokia. Mmoja wao, jina lake Agabo, akainuka kwa kuongozwa na Roho, akaonyesha, kwamba itakuwa njaa kubwa ulimwenguni mote; nayo ikawako siku za Klaudio. Ndipo, wanafunzi walipopatana, kwamba kila mtu kwa hivyo, alivyofanikiwa, atoe mali, zipelekwe za kuwatumikia ndugu waliokaa Yudea. Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli. Siku zile mfalme Herode alikuwa amekamata wengine miongoni mwao wateule, awafanyizie maovu. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Alipoona, ya kuwa Wayuda wamependezwa, akaendelea, akamkamata naye Petero, siku za mikate isiyochachwa zilipotimia. Alipokwisha kumkamata akamtia kifungoni, akaagiza vikosi vinne, kila kikosi cha askari wanne, wamlinde kwa zamu, akataka kumtia mikononi mwa watu, siku za Pasaka zitakapokuwa zimepita. Petero alipolindwa hivyo kifungoni, wateule wakamwombea kwa Mungu pasipo kuchoka. Lakini hapo, Herode alipotaka kumtoa, usiku uleule Petero alikuwa amelala katikati ya askari wawili akiwa amefungwa na mapingu mawili; nao walinzi walikilinda kifungo mlangoni. Mara malaika wa Bwana akasimama hapo karibu, nao mwanga ukamulika chumbani. Akamwamsha Petero kwa kumpiga ubavu akisema: Inuka upesi! Ndipo, mapingu yalipomwanguka mikononi. Kisha malaika akamwambia: Jifunge nguo zako, uvae navyo viatu vyako! Alipokwisha kufanya hivyo, akamwambia tena: Jivike kanzu yako, unifuate! Kisha akatoka akimfuata, asijue, kama ni kweli yaliyofanyika na malaika; maana aliwaza, ameona njozi. Wakapita zamu ya kwanza ya walinzi na ya pili, wakalifikia lango la chuma linaloelekea mjini, nalo likawafungukia lenyewe, wakatoka; walipoendelea njia tu, papo hapo ndipo, malaika alipoondoka na kumwacha. Naye Petero, moyo wake ulipomrudia, akasema: Sasa nimejua kweli ya kuwa Bwana amemtuma malaika wake, akaniokoa katika mkono wa Herode na katika mangojeo yote ya watu wa kwao Wayuda. Alipokuwa akiyawaza hayo akaifikia nyumba ya Maria, mama yake Yohana anayitwa Marko; ndimo, wengi walimokuwa wamekusanyikia kuomba. Alipogonga kilango kilichomo langoni, akaja kijakazi kusikiliza, jina lake Rode. Naye alipoutambua mtamko wa Petero hakulingua lango kwa furaha, ila akaingia mbio, akawaambia, ya kuwa Petero amesimama langoni. Nao wakamwambia: Una wazimu. Lakini alipokaza kusema, ya kuwa ndivyo, wakasema: Ni malaika wake. Petero alipofuliza kugonga, wakamfungulia, wakamwona, wakashangaa sana. Akawapungia mkono, wanyamaze; kisha akawasimulia, jinsi Bwana alivyomtoa kifungoni, akasema: Habari wapasheni nao akina Yakobo nao walio ndugu! Kisha akatoka, akaenda mahali pengine. Palipokucha, pakapatikana mahangaiko mengi kwa askari, wasijue, jinsi ya Petero yalivyowezekana. Naye Herode asipompata hapo, alipomtaka, akawaulizauliza walinzi, akaagiza, wafungwe. Kisha akaondoka Yudea, akatelemka kwenda Kesaria, akatua huko. Lakini moyoni alifikiri kuwashambulia watu wa Tiro na Sidoni; ndipo, walipomwendea wote pamoja, wakamhonga Bulasto aliyekuwa mshika funguo wa mfalme, wakamwomba, awaamue, kwa sababu walichuma vyakula vyao katika nchi ya mfalme. Siku, waliyopatania, Herode akavaa nguo ya kifalme, akakaa katika kiti cha uamuzi, akatoa maneno. Watu walipoitikia kwamba: Ni Mungu, tunayemsikia, si mtumtu tu, papo hapo malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu. Akawa akiliwa na vidudu, akakata roho. Lakini Neno la Bwana likakua na kuenea pengi. Barnaba na Sauli walipoimaliza kazi yao wakarudi toka Yerusalemu wakimchukua naye Yohana aliyeitwa Marko Katika wateule waliokuwamo Antiokia walikuwa wafumbuaji na wafunzi, akina Barnaba na Simeoni aliyeitwa Nigeri na Lukio wa Kirene na Manaeni aliyelelewa pamoja na mfalme Herode, tena Sauli. Hao walipokuwa wakimtumikia Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema: Nitengeeni Barnaba na Sauli, waifanye kazi, niliyowaitia! Ndipo, walipofunga na kuomba, wakawabandikia mikono, kisha wakawasindikiza. Kwa hivyo, walivyotumwa na Roho Mtakatifu, wakatelemka kwenda Seleukia; huko wakaingia chomboni kwenda Kipuro. Walipofika Salami wakalitangaza Neno la Mungu katika nyumba za kuombea za Wayuda. Naye Yohana alikuwa pamoja nao akiwatumikia. Wakakikata kisiwa chote wakienda kwa miguu mpaka Pafo, hapo wakaona mtu wa Kiyuda aliyekuwa mganga na mwaguaji wa uwongo, jina lake Baryesu. Huyo alikaa kwa mtawala nchi Sergio Paulo aliyekuwa mtu mwelekevu. Alipomwita Barnaba na Sauli kwa kutaka kulisikia Neno la Mungu, yule mganga Elima (kwani hii ndiyo maana ya jina lake) akawabishia mno akitaka kumpinga mtawala nchi, asije kumtegemea Mungu. Lakini Sauli anayeitwa Paulo akajaa Roho takatifu, akamkazia macho, akasema: Wewe mwana wa Msengenyaji, uliyejaa udanganyi na uovu wote, unachukizwa na wongofu wote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Sasa utaona, mkono wa Bwana ukikukamata! Utakuwa kipofu, usilione jua siku hizi! Papo hapo akaguiwa na kiwi cha macho na giza, akapapasapapasa akitafuta watu wa kumshika mkono. Mtawala nchi alipoyaona yaliyofanyika, akaustaajabu huo ufundisho wa Bwana, akamtegemea. Kisha Paulo na wenziwe wakajipakia chomboni, wakaondoka Pafo kwenda Perge katika Pamfilia; lakini Yohana akawaacha, akarudi Yerusalemu. Walipoondoka Perge, wakakata nchi, wakafika Antiokia wa Pisidia; siku ya mapumziko wakaingia nyumbani mwa kuombea, wakakaa. Mafungu ya Maonyo na ya Wafumbuaji yalipokwisha kusomwa, wakubwa wa nyumba ya kuombea wakatuma kwao kwamba: Ndugu zetu, mkiwa na neno la kuituliza mioyo ya watu lisemeni! Ndipo, Paulo alipoinuka, akawapungia mkono, akasema: Waume wa Isiraeli, nanyi mnaomcha Mungu, sikilizeni! Mungu wa watu hawa wa kwetu Waisiraeli aliwachagua baba zetu, akawakuza kuwa makundi makubwa, walipokaa ugenini katika nchi ya Misri. Kisha akaunyosha mkono wake, akawaongoza na kuwatoa kule, akawavumilia jangwani miaka kama 40. Alipokwisha poteza mataifa saba katika nchi ya Kanaani, akawapa nchi yao, waitwae. Kisha akawapa waamuzi miaka kama 450, mpaka siku za mfumbuaji Samueli. Walipotaka mfalme, Mungu akawapa Sauli, mwana wa Kisi, mtu wa shina la Benyamini, miaka 40. Tena alipokwisha kumwondoa huyo akamwinua Dawidi, awe mfalme wao; mwenyewe akamshuhudia kwamba: Nimemwona Dawidi, mwana wa Isai, kuwa mtu anayeupendeza moyo wangu; ndiye atakayeyafanyiza yote, niyatakayo. Katika uzao wake huyo Mungu akawaletea Waisiraeli mwokozi Yesu, kama alivyoagana nao. Alipokuwa hajawatokea bado, Yohana alikwisha kuwatangazia watu wote wa Isiraeli ubatizo wa kujutisha. Lakini Yohana alipoumaliza mwenendo wake akasema: Yeye, mnayeniwazia kuwa, mimi siye; lakini tazameni, anakuja nyuma yangu, ambaye hainipasi kumfungulia viatu vya miguu yake. Waume ndugu zangu, wana wa uzao wa Aburahamu, nanyi mnaomcha Mungu, Neno la wokovu huu lilitumwa kufika kwetu sisi; lakini wale wanaokaa Yerusalemu na wakubwa wao hawakumtambua huyo, wakamhukumu; ndivyo, walivyoyatimiza maneno ya Wafumbuaji yanayosomwa kila siku ya mapumziko. Ijapokuwa hawakuona neno lolote la kumwua, wakamhimiza Pilato, aangamizwe. Nao walipokwisha kuyatimiza yote, aliyoandikiwa, wakamwambua mtini, wakamzika kaburini; lakini Mungu akamfufua katika wafu. Kisha siku nyingi akaonekana kwao waliotoka pamoja naye Galilea kwenda kupanda Yerusalemu. Hao sasa ndio mashahidi wake kwenye watu wa kwetu. Nasi tunawapigia mbiu njema ya kile kiagio, baba zetu walichokipata kwamba: Mungu amekitimizia wana wetu alipomfufua Yesu. ndivyo, alivyoandikwa hata katika shangilio la pili: Wewe ndiwe Mwanangu, siku hii ya leo mimi nimekuzaa. Lakini ya kuwa amemfufua katika wafu, asirudie tena kuoza, ndivyo, alivyosema kwamba: Nitawapa ninyi magawio matakatifu ya Dawidi yanayotegemeka. Kwa hiyo anasema hata pengine: Hutamtoa akuchaye, apate kuoza. Lakini Dawidi alipokwisha kuwatumikia waliokuwako siku zile kwa mapenzi yake Mungu, alipata kulala, akawekwa mahali pa baba zake, akapata kuoza. Lakini yule Mungu aliyemfufua, hakupa kuoza. Kwa hiyo waume ndugu, litambulkane kwenu, ya kuwa ni kwa ajili yake yeye, mkipigiwa mbiu ya kwamba: Makosa yameondolea! Na tena: Yote yasiyowezekana kuondolewa kwa nguvu ya Maonyo ya Mose, kila mwenye kumtegemea Bwana anaondolewa nayo kwa nguvu yake yeye, awe mwongofu. Kwa hiyo angalieni, ninyi yasiwajie yaliyosemwa na Wafumbuaji ya kuwa: Ninyi wenye kubeza, angalieni na kustaajabu, mzizimke! Kwani mimi siku hizi nitatenda tendo, kama mtu angewasimulia tendo hilo, msingeliitikia. Walipotoka hapo, wamizimu wakawaomba, nao waambiwe maneno hayo siku ya pili ya mapumziko. Waliokuwamo nyumbani mwa kuombea walipotawanyika, Wayuda na wafuasi wengi waliomcha Mungu wakamfuata Paulo na Barnaba. Waliposema nao wakawahimiza, washikamane na magawio yake Mungu. Siku ya mapumziko iliyofuata walikusanyika wao wa mji wote, walisikie Neno la Mungu. Lakini Wayuda walipoyaona hayo makundi ya watu wakajazwa wivu, wakayabisha yaliyosemwa na Paulo na kumtukana. Ndipo, Paulo na Barnaba waliposema waziwazi pasipo woga: Ilikuwa imepasa, ninyi mwambiwe wa kwanza Neno la Mungu. Lakini mnapolitupa na kujiwazia kwamba: Uzima wa kale na kale hauwafalii, basi, twawageukia wamizimu. Kwani tumeagizwa hivyo na Bwana: Nimekuweka kuwa mwanga wa wamizimu, uwe wokovu wao hata mapeoni kwa nchi. Wamizimu walipoyasikia haya wakafurahi, wakalitukuza Neno la Bwana, wakalitegemea wote waliokuwa wamewekewa kupata uzima wa kale na kale. Ndivyo, Neno la Bwana lilivyoenea katika nchi ile yote. Lakini Wayuda waliwachokoza wanawake wakuu walioyashika matambiko yao, hata wakubwa wa mji, wakawachukua, wawashambulie akina Paulo na Barnaba, wakawafukuza, watoke mipakani kwao. Ndipo, walipowakung'utia mavumbi ya miguuni, wakaenda, wakaja Ikonio. Lakini wanafunzi wakajazwa furaha na Roho takatifu. Ikawa, walipokusanyika huko Ikonio nyumbani mwa kuombea mwa Wayuda, wakawaambia maneno yayo hayo, hata Wayuda na Wagriki wengi mno wakaja kuyategemea. Lakini Wayuda waliokataa kutii wakaichokoza mioyo ya wamizimu na kuwawazisha maovu, wachukizwe na hao ndugu. Wakakaa huko siku nyingi wakitangaza waziwazi, walivyoshikamana na Bwana, naye akayashuhudia hayo maneno, waliyoyasema ya magawio yake akitokeza vielekezo na vioja vilivyofanyizwa na mikono yao. Watu waliokuwamo mle mjini wakakosana, wengine walikuwa upande wa Wayuda, wengine upande wa mitume. Lakini wamizimu na Wayuda pamoja na wakubwa wao walitaka kuwashambulia, wawakorofishe na kuwapiga mawe. Walipoyatambua wakakimbilia miji ya Likaonia na Listira na Derbe na mingine iliyoko kandokando. Wakakaa huko wakiipiga hiyo mbiu njema. Listira kulikuwa na mtu aliyekaa hawezi miguu; ni kiwete tangu hapo, alipotoka tumboni mwa mama yake, hakuweza kwenda kamwe. Huyu alimsikiliza Paulo, alipokuwa akisema. Naye alipomkazia macho, akamwona, ya kuwa anatazamia kuponywa, akamwambia kwa sauti kuu: Inuka, usimame kwa miguu yako, inyoke! Ndipo, alipoinuka na kuruka na kuzungukazunguka. Makundi ya watu walipoona, Paulo alilolifanya, wakapaza sauti wakisema kwa Kilikaonia: Miungu imegeuka kufanana na sisi watu, ikatushukia. Wakampa Barnaba jina lake Zeu na Paulo jina lake Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kisha mtambikaji wa nyumba ya Zeu iliyokuwa nje ya mji akaleta ng'ombe na vilemba vya maua malangoni, yeye na makundi ya watu wakataka kuwachinjia ng'ombe za tambiko. Lakini mitume Barnaba na Paulo walipoyasikia wakayararua mavazi yao, wakayarukia hayo makundi, wakapaza sauti wakisema: Waume, haya mnayafanyia nini? Hata sisi tu watu wenye kufa kama ninyi. Tunawapigia mbiu njema, mwiache miungu hii ya bure, mmgeukie Mungu Mwenye uzima aliyeziumba mbingu na nchi na bahari navyo vyote vilivyomo. Siku zilizopita aliwaacha wamizimu wote, wazishike njia zao; lakini hakujitowesha kwenu, maana alifanya mema akiwapa mvua toka mbinguni na miaka ya mavuno mazuri, hivyo aliishibisha mioyo yenu vyakula na mashangilio. Wakisema hivyo, ilisalia kidogo tu, wasiweze kuwazuia hao watu wengi, wasiwachinjie ng'ombe za tambiko. Kisha Wayuda wakaja huko toka Antiokia na Ikonio, wakachokoza makundi ya watu, wakampiga Paulo mawe, wakamtoa mjini na kumburura wakidhani, amekwisha kufa. Lakini wanafunzi walipomsimamia kwa kumzungukia, akainuka, akaingia mjini. Kesho yake akatoka pamoja na Barnaba kwenda Derbe. Ule mji nao wakaupigia hiyo mbiu njema, wakapata wanafunzi wengi; kisha wakarudi kwenda Listira na Ikonio na Antiokia. Wakaishupaza mioyo ya wanafunzi, wakawahimiza, wafulize kumtegemea Bwana, wakawaambia: Inatupasa kupatwa na maumivu mengi, tukiingia katika ufalme wa Mungu. Kila mahali penye wateule wakawawekea wazee, wakawapeleka kwa Bwana, ambaye walianza kumtegemea, wakiwaombea pamoja na kufunga. Wakaikata nchi ya Pisidia, wakafika Pamfilia, wakalitangaza lile Neno mle Perge, wakatelemka kwenda Atalia. Huko wakajipakia chomboni kwenda Antiokia; ndiko, walikotoka kwa kutumwa, wenzao wakiwaombea, Mungu awaongoze kwa upole katika kazi ile, waliyokwisha kuitimiza. Walipofika wakawakusanya wateule, wakawasimulia yote, Mungu aliyoyafanya kwa kuwa nao, hata alivyowafungulia wamizimu mlango, nao wapate kumtegemea. Siku, walizokaa huko pamoja na wanafunzi, si chache. Kulikuwa na watu waliotelemka toka Yudea, wakaja huko, wakawafundisha ndugu kwamba: Hamwezi kuokoka msipotahiriwa, kama Mose alivyotuzoeza. Ikawa, Paulo na Barnaba wakabishana nao kabisa na kushindana sana. Kisha wakamwagiza Paulo na Barnaba na wenzao wengine, wapande kwenda Yerusalemu kwao mitume na wazee kwa ajili ya mshindano huu. Wakasindikizwa na wateule, wakapita Ufoniki na Samaria, wakaeleza Po pote, wamizimu walivyogeuka; hivyo wakawafurahisha sana ndugu wote. Walipofika Yerusalemu wakapokelewa nao wateule na mitume na wazee, wakayaeleza yote, Mungu aliyoyafanya kwa kuwa nao. Pakainuka waliokuwa wa chama cha Mafariseo, lakini nao walikuwa wenye kumtegemea Bwana, wakasema: Sharti watahiriwe! Sharti waagizwe kuyashika Maonyo ya Mose! Mitume na wazee wakakusanyika, walitazame neno hilo. Mashindano yalipokuwa mengi, Petero akainuka, akawaambia: Waume ndugu, ninyi mnajua, ya kuwa siku zilizopita huku kwenu Mungu alikichagua kinywa changu, wamizimu wakisikie, kinavyowapigia hiyo mbiu njema, waje kuitegemea. Naye Mungu mwenye kuitambua mioyo akawapokea wamizimu alipowapa Roho Mtakatifu, kama alivyotupa na sisi. Tena hakuna, asichowalinganisha na sisi, maana nao amewang'aza mioyo kwa vile, walivyomtegemea. Sasa mwamjaribiaje Mungu mkiwatwisha wanafunzi mzigo, ambao baba zetu hawakuweza kuuchukua, uliotushinda nasi? Lakini tunayategemea, ya kuwa tutaokolewa kwa kugawiwa na Bwana Yesu, sawasawa kama wale nao. Basi, mkutano wote ukanyamaza, wakamsikiliza Barnaba na Paulo, wakivisimulia vielekezo na vioja vyote, Mungu alivyovifanya kwa mikono yao katika wamizimu. Waliponyamaza tena, Yakobo akajibu akisema: Waume ndugu, mnisikilize! Simoni amesimulia, Mungu alivyoanza kuwachagua wamizimu, alipatie Jina lake kundi la watu humo namo. Nayo maneno ya Wafumbuaji huelekeza papo hapo, kama ilivyoandikwa kwamba: Hayo yakiisha, nitarudi, nikijenge tena kibanda cha Dawidi kilichoanguka; hapo palipojenguka nitapajenga tena, nipate kukisimamisha tena, maana watu waliosalia wote wapate kumtafuta Bwana pamoja na wamizimu wote waliotangaziwa Jina langu. Ndivyo, asemavyo Bwana anayeyafanya haya. Yanatambulikana toka kale. Kwa hiyo mimi naona: Wanaotoka kwa wamizimu na kumgeukia Mungu tusiwachukuze mizigo isiyofaa, ila tuwaandikie kwamba: Miiko ni hii tu: Kutambikia mizimu, maana huchafua moyo wa mtu, tena ugoni, tena nyamafu, tena damu. Kwani toka kale hata sasa Mose anao mijini mote wanaoyatangaza maneno yake, tena katika nyumba za kuombea yanasomwa kila siku ya mapumziko. Ndipo, mitume na wazee walipopatana na wateule wote kuchagua wenzao wengineo na kuwatuma kwenda Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda anayeitwa Barsaba na Sila, waliojua kuongoza ndugu. Wakaandika barua, waipeleke mikononi mwao, ni ya kwamba: Sisi mitume na wazee tunawaamkia kindugu ninyi ndugu zetu huko Antiokia na Ushami na Kilikia mliotoka kwa wamizimu. Tumesikia, ya kuwa wengine watu, tusiowaagiza neno, wamewahangaisha kwa maneno ya kuwatia wasiwasi mioyoni mwenu. Tukakusanyika kwa hivyo, tulivyo na moyo mmoja, tukapatana kuchagua watu na kuwatuma kwenu pamoja na wenzetu akina Barnaba na Paulo, tunawapenda, kwani ni watu waliojitoka wenyewe kwa ajili ya Jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, tumemtuma Yuda na Sila, nao watawaelezea kwa vinywa maneno yaya haya. Kwani sisi na Roho Mtakatifu tumepatana, tusiwatwike mzigo kuliko yaleyale yanayofaa, mshike mzio wa nyama za tambiko na wa damu na wa nyamafu na wa ugoni. Mkijikataza mambo haya mtafanya vema. Kaeni vema! Salamu. Kisha wakasindikizwa, wakatelemka kwenda Antiokia, wakawakusanya wao wote wa hilo kundi, wakawatolea ile barua. Wale walipoisoma wakafurahi kwa ajili ya matulizo. Hata Yuda na Sila waliokuwa wafumbuaji wenyewe wakawatuliza ndugu na kuwaambia mengi, wakawashupaza. Walipokwisha kukaa kitambo walisindikizwa na ndugu kwa hivyo, walivyopatana, warudi kwao waliowatuma. Lakini Sila alipendezwa kukaa huko. Naye Paulo na Barnaba wakakaa Antiokia wakilifundisha Neno la Bwana na kuipiga hiyo mbiu njema pamoja na wenzao wengi. Siku zilipopita, Paulo akamwambia Barnaba: Turudi tena, tuwakague ndugu mijini mote, tulimolitangaza Neno la Bwana! Lakini Barnaba alitaka kumchukua naye Yohana aliyeitwa Marko. Lakini Paulo alidhani, haifai kumchukua aliyewatoroka huko Pamfilia, asifuatane nao kazini. Kwa hiyo wakabishana kwa ukali, hata wakatengana yeye na mwenziwe; Barnaba akamchukua Marko, akaingia chomboni kwenda Kipuro, naye Paulo akamchukua Sila, akaondoka akiombewa na ndugu, Mungu awaongoze kwa upole. Akaipita nchi ya Ushami na Kilikia, akawashupaza wateule. Akafika Derbe na Listira; huko kulikuwa na mwanafunzi, jina lake Timoteo, mwana wa mwanamke wa Kiyuda aliyemtegemea Bwana, lakini baba alikuwa Mgriki. Kwa kuwa huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokuwamo mle Listira na Ikonio, Paulo alimtaka, aondoke kwenda naye. Akamchukua, akamtahiri kwa ajili ya Wayuda waliokuwa katika miji ile, kwani wote walimjua, ya kuwa baba yake alikuwa Mgriki. Walipozunguka katika miji ile wakawafundisha kuishika ile miiko iliyoagizwa nao mitume na wazee wa Yerusalemu. Hivyo wateule wakapata nguvu za kumtegemea Bwana, wakawa wengi zaidi kwa kuongezwa kila siku. Wakaikata nchi ya Furigia na ya Galatia wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasiliseme Neno lao katika Asia. Walipofika Misia, wakajaribu kwenda Bitinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa. Basi wakapita Misia, wakatelemka, wakafika Tiroa. *Huko Paulo akatokewa na njozi usiku, akaona mtu wa Makedonia, amesimama na kumbembeleza kwamba: Vuka, uje Makedonia, utusaidie! Alipokwisha kuiona njozi hiyo, papo hapo tukatafuta, jinsi tutakavyovuka, tuje Makedonia, maana sote tumejua kweli, ya kuwa ni Mungu aliyetuita, tuje, tuwapigie hiyo mbiu njema. Tukaondoka Tiroa, tukaingia chomboni, tukaenda kwa tanga moja Samotirake; kesho yake tukafika Mji Mpya. Toka huko tukafika Filipi, ni mji wa mbele wa upande huo wa Makedonia, tena ndimo, Waroma walimotua. Tulipokuwa tumekaa mjini mle siku kidogo tukatoka langoni kwenda nje siku ya mapumziko, tukaenda kando ya mto, tulipowazia kuwa pao pa kuombea. Ndipo, tulipokaa, tukisema na wanawake waliokusanyika. Palikuwapo mwanamke, jina lake Lidia; alitoka mji wa Tiatira, akawa mchuuzi wa nguo za kifalme. Kwa sababu alimcha Mungu, akasikiliza. Naye Bwana akamfunulia moyo, ayashike yaliyosemwa na Paulo. Alipokwisha kubatizwa pamoja nao waliokuwamo mwake akatubembeleza na kusema: Kama mmeniona mimi kwamba: Ni mwenye kumtegemea Bwana, mwingie mwangu, mkae! Ndivyo, alivyotushurutisha.* *Ikawa, sisi tulipokwenda kuomba, tukakutana na kijakazi mwenye pepo ya kuagua. Naye aliwachumia mabwana zake mali nyingi na uaguzi wake. Pote, tulipokwenda, akatufuata, Paulo na sisi, akapaza sauti akisema: Watu hawa ndio watumwa wake Mungu alioko huko juu, nao huwatangazia njia ya wokovu. Alipovifanya siku nyingi, vikamwumiza Paulo, akageuka, akamwambia yule pepo: Nakuagiza wewe kwa Jina la Yesu Kristo, umtoke! Naye akamtoka saa ileile. Lakini mabwana zake walipoona, ya kuwa chumo lao la mali limewapotea, wakamshika Paulo na Sila, wakawaburura, wakaenda nao sokoni kwa wakubwa wa mji. Wakawapeleka kwa mabwana wakubwa, wakasema: Watu hawa wanauchafua mji wetu; ni Wayuda, hufundisha desturi zilizo mwiko kwetu kuzipokea au kuzifanya sisi tulio Waroma. Watu wengi walipoinuka kuwaendea kwa nguvu, mabwana wakubwa wakawapokonya mavazi yao, wakaagiza, wapigwe. Walipokwisha kuwapiga viboko vingi wakawatia kifungoni, wakamwagiza mlinda kifungo, awatie mahali pasipoingilikana. Naye alipolipata agizo hili akawatia katika chumba cha ndani kabisa, tena miguu yao akaitia mikatale. Lakini usiku wa manane Paulo na Sila wakamwomba Mungu na kumwimbia, wafungwa wenzao wakiwasikiliza. Papo hapo nchi ikatetemeka sana, hata misingi ya kifungo ikatikisika; mara milango yote ikafunguka, hata minyororo yao wote ikakatika. Mlinda kifungo akazinduka, akaona, milango ya kifungo iko wazi, akachomoa upanga, akataka kujiua, kwani alidhani, wafungwa wametoroka. Lakini Paulo akamkemea na kupaza sauti akisema: Usijifanyie kiovu! Kwani sisi sote tupo hapa. Akaagiza, taa ije, akarukia ndani na kutetemeka, akamwangukia Paulo na Sila. Alipowapeleka nje na kuwauliza: Bwana zangu, inayonipasa kuyafanya, nipate kuokoka ndiyo nini? wakasema: Mtegemee Bwana Yesu! Ndivyo, utakavyookoka wewe nao waliomo nyumbani mwako. Wakamwambia Neno lake Mungu yeye nao wote waliokuwamo mwake.* Akawakaribisha saa ileile ya usiku, akawaosha madonda ya mapigo yao, akabatizwa papo hapo yeye nao wote waliokuwa wake. Kisha akawaingiza mwake, akawaandalia meza, akashangilia yeye nao wa nyumbani mwake wote, ya kuwa wamepata kumtegemea Mungu. Kulipokucha, mabwana wakubwa wakawatuma wale askari waliowapiga, wamwambie: Wafungue watu wale! Mlinda kifungo alipomwambia Paulo maneno haya kwamba: Mabwana wakubwa wametuma watu, mfunguliwe; sasa tokeni mwende na kutengemana! Paulo akawaambia: Wametupiga mbele ya watu pasipo kutuhukumu sisi tulio Waroma na kututia kifungoni. Sasa je? Wanataka kutukimbiza na kufichaficha? Sivyo, sharti waje wenyewe, watutoe! Askari waliowapiga walipowaambia mabwana wakubwa maneno haya, wakashikwa na woga kwa kusikia, ya kuwa ndio Waroma. Wakaja, wakawabembeleza, wakawatoa, wakawaomba sana, watoke mjini mle. Ndipo, walipotoka kifungoni, wakaingia nyumbani mwa Lidia; walipokwisha kuonana na ndugu na kuwatuliza mioyo wakaondoka. Wakapita katika Amfipoli na Apolonia, wakafika Tesalonike palipokuwa na nyumba ya kuombea ya Wayuda. Kama Paulo alivyozoea, akaingia humo, akaongea nao maneno ya Maandiko siku tatu za mapumziko. Akawafunulia na kuwaelezea, ya kuwa Kristo alipaswa na kuteswa na kufufuka katika wafu, akawaambia: Yesu, ambaye ninawatangazia habari zake, yuyu huyu ndiye Kristo. Wamoja wao wakashindwa mioyoni, wakashikamana nao akina Paulo na Sila; nao waliotoka kwa Wagriki wenye kumcha Mungu walikuwa wengi mno, hata wanawake wenye cheo hawakuwa wachache. Lakini Wayuda wakaingiwa na wivu, wakajichukulia kikundi cha majitu mabaya wasiokuwa na kazi; hao wakakusanya kundi zima la watu, kisha wakauchafua mji wote, wakaisogeleasogelea nyumba ya Yasoni, wakawatafuta, wawapeleke kwenye kundi lilelile. Wasipowaona wakamburura Yasoni na ndugu wengine, wakaenda nao kwa wakubwa wa mji wakipiga kelele na kusema: Watu hawa waliouchafua ulimwengu wamefika hata hapa, naye Yasoni ndiye aliyewafikiza. Hawa wote huyakanusha maagizo ya Kaisari wakisema: Mfalme ni mwingine, ni Yesu. Wakahangaisha watu wengi, hata wakubwa wa mji wakayasikia. Hao walipokwisha kumtoza Yasoni na wenzake mali zilizowatosha, wakawaacha, waende zao. Ndipo, ndugu walipomsindikiza Paulo na Sila papo hapo na usiku kwenda Beroya. Walipofika huko wakaingia nyumbani mwa kuombea mwa Wayuda. Hao walikuwa wema kuliko wale wa Tesalonike, wakalipokea Neno kwa mioyo iliyolipenda sana, kila siku wakayachunguza Maandiko, waone, kama ndivyo yalivyo kweli. Hivyo wenzao wengi wakaja kumtegemea Bwana, vile vile hata kwa Wagriki wanawake na waume wenye cheo hawakuwa wachache. Lakini Wayuda wa Tesalonike walipotambua, ya kuwa Neno lake Mungu linatangazwa na Paulo hata huko Beroya, wakaja, wakawahangaisha watu nako huko. Papo hapo ndugu wakamsindikiza Paulo, wakamfikisha pwani. Lakini Sila na Timoteo wakakaa huko. Lakini wale waliomsindiza Paulo wakaenda naye mpaka Atene. Walipokwisha kupata maagizo ya kuwapelekea akina Sila na Timoteo, kwamba waje upesi sana kwake, wakaenda zao. *Paulo alipowangoja huko Atene akaumia rohoni mwake akiona, mji ulivyojaa miungu ya kutambikia. Akaongea nao Wayuda na watu wenye kumcha Mungu nyumbani mwa kuombea. Hata sokoni alisema kila siku na wale, aliowakuta hapo. Lakini kulikuwako wenye ujuzi wa chama cha Waepikurio na wa chama cha Wastoiko, wakabishana naye, wengine wakasema Mpuzi huyu anataka kusema nini? Wengine tena wakasema: Anaonekana kuwa mtangazaji wa miungu migeni. Kwani alikuwa anawapigia hiyo mbiu njema ya Yesu na ya ufufuko. Ndipo, walipomshika, wakampeleka panapoitwa Areopago, wakamwuliza: Twaweza kutambua, yalivyo hayo mafundisho yako mapya, unayoyasema? Kwani unaingiza maneno mageni masikioni mwetu. Sasa twataka kutambua, hayo yatakapoelekea. Lakini wenyeji wote wa Atene na wageni waliotua humo hakuna, walichokitunukia kuliko kusema au kusikia yaliyo mapya. Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema: Enyi waume wa Atene, po pote ninawaona ninyi, mnavyotambikia miungu. Kwani nilipozunguka na kupatazama pa kuombea penu nikaona pa kuchinjia ng'ombe za tambiko palipoandikwa: Penye Mungu asiyetambulikana. Basi, huyo, mnayemtumikia pasipo kumjua, ndiye, ninayewatangazia. Mungu aliyeuumba ulimwengu navyo vyote vilivyomo hakai katika nyumba za kuombea zilizojengwa na mikono ya watu, kwani yeye ni Bwana wa mbingu na wa nchi. Naye hatumikiwi na mikono ya watu, tena hatumii kitu cho chote, kwani yeye mwenyewe ndiye aliyewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Kwa tendo lake yeye watu wa mataifa yote wametoka kwa mmoja, wakakaa ko kote katika nchi zote zilizoko nchini; akawagawia huko kale siku zao za kuwapo, akawakatia nayo mipaka ya makao yao. Alitaka, wamtafute Mungu, kama wanaweza kumnyatia, mpaka wamwone. Namo miongoni mwetu sisi hamna hata mmoja tu, ambaye anamkalia mbali. Kwani yeye ndiye, tunayekalia, tunayeendea, tunayekuwa naye, kama watunga nyimbo walivyosema hata kwenu kwamba: Uzao wake ndio sisi. Basi, tukiwa uzao wake Mungu, haifai kumfananisha Mungu na maumbo ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe yaliyotengenezwa kwa uwezo na kwa mawazo ya kimtu. Siku za kujikalia tu na kupumbaa Mungu ameziacha tu, zipite; lakini sasa anawaagiza watu wote po pote, wajute. Kwani ameweka siku, atakapompa mtu mmoja, aliyemwonea kazi hiyo, auhukumu ulimwengu wote kwa wongofu; lakini kwanza anawahimiza wote, wamtegemee, maana amemfufua katika wafu. Walipousikia ufufuko wa wafu, wengine wakamfyoza, wengine wakasema: Tunataka kukusikia na siku nyingine, utuelezee jambo hilo. Ndipo, Paulo alipotoka katikati yao. Lakini walikuwako waliogandamana naye, wakaja kumtegemea Bwana. Miongoni mwao alikuwamo mtu wa Areopago, ndiye Dionisio, tena mwanamke, jina lake Damari, na wengine waliokuwa pamoja nao.* Kisha Paulo akatoka Atene, akafika Korinto. Akaona Myuda mmoja, jina lake Akila, aliyezaliwa Ponto; naye alikuwa amekuja juzijuzi toka Italia pamoja na mkewe Puriskila, kwa sababu Kaisari Klaudio aliagiza, Wayuda wote watoke Roma. Akafikia kwao, kwa sababu kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi; maana walikuwa mafundi wa kushona mahema. Lakini kila siku ya mapumziko akabishana nao Wayuda na Wagriki nyumbani mwa kuombea, akawafundisha na kuwashinda. Lakini Sila na Timoteo walipofika toka nchi ya Makedonia, Paulo akafuliza kulitangaza Neno akiwashudia Wayuda, ya kuwa Yesu ndiye Kristo. Lakini walipopingamana naye na kumtukana, akawakung'utia mavumbi ya nguo zake, akawaambia: Damu zetu zitavijia vichwa vyenu! Mimi simo, ila nimetakata nikienda tangu sasa kwao wamizimu. Akaondoka mle, akaingia nyumbani mwa mtu mwenye kumcha Mungu, jina lake Tiro Yusto, ambaye nyumba yake ilikuwa imepakana na nyumba ya kuombea. Lakini Krispo aliyekuwa mkubwa wa nyumba ya kuombea alimtegemea Bwana pamoja na waliokuwamo nyumbani mwake wote. Hata wenyeji wa Korinto wengi walipovisikia wakamtegemea, wakabatizwa. Bwana akamwambia Paulo kwa njozi usiku: Usiogope, tangaza tu, usinyamaze! Kwani mimi niko pamoja nawe, hakuna atakayekushika, akufanyie maovu. Kwani humu mjini ninao watu wengi. Akakaa huko mwaka na miezi sita akifundisha kwao Neno la Mungu. Lakini Galioni alipokuwa bwana mkubwa wa nchi ya Akea, Wayuda wakapatana kumwunukia Paulo, wakampeleka bomani, wakasema: Huyu anawahimiza watu kumcha Mungu na kuyabeza Maonyo yake. Naye Paulo alipotaka kukifumbua kinywa chake, Galioni akawaambia Wayuda: Nyie Wayuda, mtu huyu kama amekosa kwa kufanya kibaya cho chote, ingalifaa kuwasikiliza vema. Lakini kama ni mabishano tu kwa ajili ya maneno na majina na maonyo ya kwenu, myatazame wenyewe! Mambo kama haya mimi sitaki kuyaamua. Akawafukuza bomani. Ndipo, wote walipomkamata Sostene, mkubwa wa nyumba ya kuombea, wakampiga mbele ya boma; lakini nayo hayo Galioni hakuyatazama. Paulo alipokwisha kukaa huko tena siku nyingi akaagana na ndugu, akatweka kwenda Ushami, Puriskila na Akila wakiwa pamoja naye; kwanza akanyoa kichwa kule Kenkerea, kwani alikuwa amejitia mwiko. Walipofika Efeso, akawaacha huko; naye mwenyewe akaingia nyumbani mwa kuombea, akaongea na Wayuda. Lakini walipombembeleza, akae kwao kitambo, hakuwaitikia, ila akaagana nao akisema: Sikukuu itakayokuja sharti niimalizie Yerusalemu, lakini Mungu akitaka, nitarudi kwenu tena. Alipoondoka Efeso, akatweka, akafika Kesaria, akapanda kuamkiana na wateule; kisha akatelemka kwenda Antiokia. Alipokwisha kukaa huko siku kidogo akaondoka tena, akakata nchi ya Galatia na ya Furigia na kuingia mji kwa mji akiwashupaza wanafunzi wote. Kulikuwa na Myuda, jina lake Apolo, aliyezaliwa Alekisandria; alikuwa na nguvu ya kusema, tena nguvu yake ilitoka katika utambuzi wa Maandiko; naye akafika Efeso. Huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana, akashurutishwa na Roho kusema na kuyafundisha mambo ya Yesu, yalivyo kweli, lakini aliujua ubatizo wa Yohana tu. Huyo alipoanza kutangaza nyumbani mwa kuombea waziwazi, Puriskila na Akila wakamsikia nao, wakampokea, wakamfunulia vema njia ya Mungu, aijue kabisa. Naye alipotaka kuvuka kwenda Akea, ndugu wakamtia moyo, wakawaandikia wanafunzi, wampokee. Alipofika huko akawasaidia sana waliogawiwa kumtegemea Bwana. Kwani aliwashinda sana Wayuda mbele za watu wote akionyesha na kuyaeleza Maandiko, ya kuwa Yesu ni Kristo. Ikawa, Apolo alipokuwako Korinto, Paulo akazunguka hapo penye milima, kisha akafika Efeso, akaona wanafunzi wengine, akawauliza: Mmepewa Roho takatifu mlipoanza kumtegemea Bwana? Nao wakamjibu: Hapana, hatujasikia, kama iko Roho takatifu. Alipowauliza: Mmebatizwa ubatizo gani? wakasema: Tumebatizwa ubatizo wa Yohana. Ndipo, Paulo aliposema: Yohana alibatiza ubatizo wa kujutisha akiwaambia watu, wamtegemee atakayekuja nyuma yake, naye ndiye Yesu. Walipoyasikia wakabatiziwa Jina la Bwana Yesu. Paulo alipowabandikia mikono, Roho Mtakatifu akawajia, akasema misemo migeni na kufumbua. Nao wote walikuwa waume kama kumi na wawili. Alipoingia nyumbani mwa kuombea, akapiga mbiu waziwazi yapata miezi mitatu, akaongeana nao mambo ya ufalme wa Mungu na kuwashinda. Lakini palipopatikana wenye mioyo migumu waliokataa kutii, walipoifyoza ile njia mbele ya watu waliokusanyika hapo, akawaacha, akawatenga nao wanafunzi, akaongea na watu kila siku katika shule ya Tirano. Vikawa hivyo kama miaka miwili; nao wote waliokaa Asia, Wayuda na Wagriki, wakapata kulisikia Neno la Bwana. Mungu akaifanyisha mikono ya Paulo matendo ya nguvu yasiyokuwapo hata kale. Kwa hiyo watu waliitwa hata miharuma na mishipi ya mwilini pake, wakawapelekea wagonjwa; ndipo, magonjwa yao yalipowaacha nao pepo wabaya wakawatoka. Kulikuwa na wapunga pepo wa Kiyuda waliozunguka hapo, wakajaribu kuwatajia waliopagawa na pepo wabaya Jina la Bwana Yesu, wakisema: Nawaapiza kwa nguvu ya Yesu, Paulo anayemtangaza. Nao waliovifanya hivyo walikuwa wana saba wa Sikewa aliyekuwa mtambikaji mkuu wa Kiyuda. Lakini pepo mbaya akawajibu: Yesu ninamtambua, naye Paulo ninamjua. Lakini ninyi, m wa nani? Kisha yule mtu mwenye pepo mbaya akawarukia, akawakamata wawili, akawafanyizia vibaya kwa nguvu zake, mpaka wakakimbia mle nyumbani wenye uchi na wenye madonda. Haya yakatambulikana kwa Wayuda na kwa Wagriki wote waliokaa Efeso, nao wote wakashikwa na woga, lakini Jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Ndipo, wengi wao walioanza kumtegemea walipokuja kuyaungama matendo yao wakiyajutia. Nao wengi wao waliofanya kazi za uganga wakavikusanya vyuo vyao, wakaviteketeza mbele yao wote. Wakazihesabu fedha zilizotumiwa, walipovinunua, wakaona, zilikuwa fedha 50000. Hivyo Neno likakua, likapata nguvu kwa uwezo wa Bwana. Hayo yalipomalizika, Paulo aliwaza moyoni kuzunguka katika Makedonia na Akea, apate kwenda Yerusalemu, akasema: Nikiisha kwenda huko, sharti niuone hata Roma! Akatuma wawili waliomtumikia, Timoteo na Erasto, watangulie kwenda Makedonia, mwenyewe akakawia kidogo Asia. Lakini siku zile ikawako kondo isiyokuwa ndogo kwa ajili ya hiyo njia. Kwani kulikuwa na mfua fedha, jina lake Demetirio, aliyekuwa akitengeneza vijumba vya fedha kwa mfano wa nyumba ya kumwombea Artemi; ndivyo, alivyowapatia mafundi wengi mali nyingi. Hao akawakusanya na wengine waliowafanyia kazi, akasema: Waume, mmejua: kazi hii ni chumo letu. Tena mnaona, pengine mnasikia, ya kuwa si kwenu Efeso tu, ila hata katika nchi zote za Asia ndiko, huyu Paulo anakohimiza watu na kugeuza mioyo ya makundi mazima ya watu akisema: Miungu iliyofanyika kwa mikono siyo. Lakini linalotuogopesha si hilo tu la kwamba: Uchumi wetu utatoweka, ila hata patakatifu pa Artemi aliye mungu wetu wa kike mkuu patabezwa kuwa si kitu. Tena pataangamia ujumbe wake mkuu unaotambikiwa na watu wote wa Asia na wa ulimwengu. Walipoyasikia, makali yakawajaa, wakapiga kelele wakisema; Mkuu ni Artemi wa Waefeso! Mji ukajaa machafuko, wakapiga mbio wote pamoja kwenda penye machezo, wakawakamata hapo na kuwaburura akina Gayo na Aristarko waliokuwa Wamakedonia, kwani waliandamana na Paulo. Paulo alipotaka kuwatokea watu, wanafunzi wakamzuia; nao wakubwa wa nchi za Asia wengine waliokuwa rafiki zake wakatuma mtu kwake, wakamtisha, asijitoe kwenda penye machezo. Hapo walikuwa wanapiga kelele, wengine hivi, wengine hivi. Watu waliokusanyika hapo walikuwa wamevurugika, wengi hawakujua kilichowakusanya. Watu wengine wakamshika Alekisandro, Wayuda waliyemsogeza, aje mbele. Naye Alekisandro akawapungia mkono, akataka kujikania mbele ya makutano; lakini walipomtambua, ya kuwa ni Myuda, wakapiga kelele wote pamoja kwa sauti moja kama saa mbili kwamba: Mkuu ni Artemi wa Waefeso! Mwandishi wa mji alipowanyamazisha wao wa makundi, akasema: Waume wa Efeso, yuko mtu asiyetambua kwamba: Mji wa Efeso ndio unaoilinda nyumba ya kumwombea Artemi aliye mkuu nao mfano wake uliotoka mbinguni? Basi, kwa kuwa haya hayabishiki, imewapasa ninyi kutulia, msifanye neno kwa kikaka. Kwani mmewaleta watu hawa wasionyang'anya vilivyomo nyumbani mwa kuombea, wala hawakumbeza mungu wetu. Kama Demetirio na mafundi wenziwe wako na neno la kusuta mtu, siku za uamuzi ziko, hata waamuzi wako, basi, na wasutane! Lakini mkiwa na neno jingine-jingine, litatimizwa mbele ya wale waliochaguliwa wa kazi hiyo. Kwani tunajiponza kusutiwa ugomvi kwa ajili ya matata haya ya leo; tena hatutakuwa na neno la kujikania sisi kwa ajili ya kondo hii. Alipokwisha kusema hivyo akauvunja mkutano. Lile fujo lilipotulia, Paulo akatuma watu kuwaita wanafunzi, akawatuliza mioyo, akaagana nao, akaondoka kwenda Makedonia. Akapita pande zile akiwatuliza mioyo na kuwaambia maneno mengi, kisha akafidka Ugriki. Akakaa huko miezi mitatu. Alipotaka kuingia chomboni, aende Ushami, Wayuda walimlia njama. Kwa hiyo akapendezwa kurudi na kupita Makedonia. Waliofuatana naye mpaka Asia ni Sopatiro, mwana wa Puro wa Beroya, na Aristarko na Sekundo wa Tesalonike na Gayo wa Derbe na Timoteo; tena Tikiko na Tirofimo wa Asia. Hao walitangulia, wakatungoja Tiroa. Siku za mikate isiyotiwa chachu zilipopita, nasi tukatweka, tukaondoka Filipi, tukawafikia huko Tiroa siku ya tano, tukaa huko siku saba. Siku ya kwanza ya juma tulipokuwa tumekusanyikia kumegeana mkate, Paulo akasema nao; kwa sababu alitaka kuondoka kesho yake, akaendelea kusema mpaka usiku wa manane. Mkawa na taa nyingi katika chumba cha juu, tulimokuwa tumekusanyika. Mlikuwa na kijana, jina lake Eutiko, alikuwa amekaa dirishani, akasinzia mno. Paulo alipofuliza kusema, akashindwa na usingizi, akaanguka toka dari ya tatu mpaka chini, akainuliwa amekufa. Lakini Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema: Msipige makelele! Kwani roho yake ingalimo mwake. Akapanda tena, akamega mkate, akala, akaongea mengi nao, mpaka kulipopambazuka. ndivyo, alivyotoka huko. Lakini yule kijana walimleta, yuko mzima, kwa hiyo mioyo yao ikawatulia kabisa. Lakini sisi tulitangulia kuingia chomboni, tukatweka kwenda Aso; ndiko, tulikotaka kumpakia Paulo. Kwani alikuwa ametuagiza hivyo; mwenyewe alitaka kufika huko kwa miguu. Naye alipokutana nasi huko Aso, tukampakia, tukafika Mitilene. Tukatweka huko, kesho yake tukaelekea Kio; kesho kutwa tukatia nanga Samo, tukakaa Tirogilio, mtondogoo tukafika Mileto. Kwani Paulo alitaka kupita Efeso kwa chombo, asipate kukawia katika Asia, maana alikwenda mbiombio, kwa sababu alitaka ikiwezekana, kuila sikukuu ya Pentekote huko Yerusalemu. *Lakini toka Mileto alituma mtu Efeso kuwaita wazee wa wateule. Hao walipofika kwake, akawaambia: Ninyi mnajua, nilivyokaa nanyi siku zote tangu siku ya kwanza, nilipofika Asia: nimemtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, hata nilipoulizwa, hata nilipojaribiwa na Wayuda mara kwa mara, wakininyatia. Hakuna neno lenye kufaa, nililowanyika nikiacha kulitangaza, tena sikuacha kuwafundisha mkikusanyika au nikienda nyumba kwa nyumba. Kwa ushahidi wangu nimewahimiza Wayuda na Wagriki, wajute na kurudi kwake Mungu, tena wamtegemee Bwana wetu Yesu. Sasa tazameni, kwa hivyo, nilivyofungwa na Roho, ninakwenda Yerusalemu, nisijue yatakayonipata huko. Naijua hii tu, ya kuwa Roho Mtakatifu hunishuhudia mijini mote, nifikamo, kwamba: Mapingu na maumivu yananingoja. Lakini ninajiwazia kwamba: Si kitu, mwenyewe nikiangamia; lakini kilicho kitu, ni kuumaliza mwendo wangu na utumishi wangu, niliopewa na Bwana Yesu, niushuhudie Utume mwema wa gawio lake Mungu. Sasa tazameni, mimi ninajua, ya kuwa hamtauona tena uso wangu ninyi nyote, ambao nilipita kwao na kuutangaza ufalme. Kwa hiyo ninawaambia waziwazi siku hii ya leo kwamba: Ninyi nyote hakuna, ambaye ninawiwa naye damu ya mtu. Kwani sikuacha kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu. Jilindeni wenyewe na kikundi chote! Kwani Roho Mtakatifu amewaweka, mwe wakaguzi wao, mwachunge wateule wake Mungu, aliojichumia kwa kuitoa damu yake mwenyewe. Mimi najua: Nitakapokwisha kuondoka, wataingia chui wakali kwenu wasiowaonea huruma wao wa kikundi hiki. Tena miongoni mwenu wenyewe watainuka watu wakaofundisha mapotovu, wapate kuwavuta nao walio wanafunzi, wawaandamie. Kwa hiyo kesheni na kukumbuka, ya kuwa miaka mitatu sikuacha usiku na mchana kumwonya kila mmoja kwa kutoa machozi! Sasa hivi ninawaweka mikononi mwake Mungu, awagawie Neno lake linaloweza kuwajenga na kuwapa fungu kwao wote waliotakaswa. Sikutaka fedha au dhahabu au mavazi ya mtu. Mnatambua wenyewe: hii mikono yangu imetumika kunichumia yaliyotulisha mimi na wenzangu waliokuwa pamoja nami. Kwangu mimi nimewaonyesha yote, ya kuwa imetupasa kusumbukia kazi vivyo hivyo, tupate kuwasaidia wanyonge, tukiyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, aliyoyasema mwenyewe: Kumpa mtu huna upato kuliko kupewa. Alipokwisha kusema hivyo akapiga magoti pamoja nao wote, akaomba. Wote wakalia sana, wakamkumbatia Paulo lshingoni, wakamnonea. Lililowasikitisha zaidi ni neno lile, alilolisema, ya kuwa hawatamwona tena uso kwa uso. Kisha wakamsindikiza hata chomboni.* Lakini tulipokwisha kuagana nao tukatweka na kukielekeza chombo kwenda Ko kwa tanga moja; tulipofika, kesho yake tukaenda hapo Rodo; toka hapo tukafika Patara. Tukaona chombo cha kuvukia hata Ufoniki, tukajipakia humo, tukatweka. Tulipokuona kule Kipuro tukakuacha kushotoni, tukaendelea mpaka Ushami, tukashukia Tiro; kwani ndiko, chombo kilikoagiziwa kuipakua mizigo yake. Tulipowaona wanafuanzi tukakaa lhuko siku saba. Nao wakamwambia Paulo kwa nguvu ya Roho, asipande kwenda Yerusalemu. Lakini tulipoziishiliza siku zetu tukaondoka kwenda zetu; wakatusindikiza wote pamoja na wanawake na watoto mpaka weuni pa mji; hapo wakapiga magoti pwani, wakatuombea. Tukaagana nao, tukaingia chomboni, lakini wale wakarudi kwao. Nasi tulipokwisha kuimaliza safari ya baharini tukatoka Tiro, tukafika Putolemai, tukawaamkia ndugu, tukakaa kwao siku moja. Kesho yake tukaondoka, tukafika Kesaria, tukaingia nyumbani mwa mpiga mbiu njema Filipo aliyekuwa miongoni mwao wale saba, tukakaa kwake. Mtu huyu alikuwa na wana wa kike wanne, walikuwa wasichana wenye kufumbua. Nasi tulipokaa siku nyingi kwake, pakashuka mfumbuaji toka Yudea, jina lake Agabo. Akatujia, akauchukua mshipi wa Paulo, akajifunga miguuni na mikono, akasema: Ndivyo, asemavyo Roho Mtakatifu: Mwenye mshipi huu Wayuda watamfunga Yerusalemu vivyo hivyo, wamtie mikononi mwa wamizimu. Tulipoyasikia haya sisi na wenyeji wa hapo tukambembeleza, asipande kwenda Yerusalemu. Ndipo, Paulo alipojibu: Huku kulia kwenu na kuniponda moyo kuna maana gani? Kwani mimi nimejielekeza siko kufungwa tu, ila hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya Jina la Bwana Yesu. Alipokataa kutusikia, tukanyamaza tukisema: Bwana ayatakayo na yafanyike! Siku hizi zilipopita, tukatengeneza yote, tukapanda kwenda Yerusalemu. Kulikuwa na wanafunzi Kesaria waliofuatana nasi, wakatupeleka kwa mtu aliyeitwa Mnasoni wa Kipuro aliyekuwa mwanafunzi wa kale, tufikie kwake. Tulipofika Yerusalemu, ndugu wakatupokea kwa furaha. Kesho yake Paulo akaingia mwa Yakobo pamoja nasi, nao wazee wote walikuwamo. Akawaamkia, akawasimulia moja kwa moja mambo yote, Mungu aliyoyafanya kwa wamizimu kwa ile kazi yake, aliyoitumikia. Walipoyasikia wakamtukuza Mungu, wakamwambia Paulo: Ndugu yetu, unaona, ya kuwa Wayuda walioanza kumtegemea Bwana ni elfu nyingi na nyingi, hao wote hujikaza kuyashika Maonyo. Lakini kwa ajili yako wewe wameambiwa ya kwamba: Unawafundisha Wayuda wote wanaokaa kwa wamizimu, wambeze Mose, ukiwaambia, wasiwatahiri watoto, wala wasiyafuate mambo yaliyo mazoezo tu. Basi, iko nini inayofaa? Sharti kundi hilo zima likusanyike, kwani hawatakosa kusikia, ya kuwa umekuja. Kwa hiyo ufanye, tutakavyokuambia! Tunao waume wanne wenye jambo, waliloliagana na Mungu. Wachukue hao ujieue pamoja nao, uwalipie, wanyolewe vichwa! Hivyo wote watatambua, ya kuwa waliyoambiwa kwa ajili yako ni uwongo tu, ya kuwa wewe mwenyewe unaendelea na kuyashika Maonyo. Lakini kwa ajili ya wamizimu walioanza kumtegemea Bwana tumewaandikia, tulivyopatana ya kwamba, waushike mzio wa nyama za tambiko na wa damu na wa nyamafu na wa ugoni. Ndipo, Paulo alipowachukua wale watu, kesho yake akaeuliwa pamoja nao, akapaingia Patakatifu, akatangaza, siku za weuo wao zitakapomalizika, kwamba ni hapo, kila mmoja atakapokwisha kutolewa kipaji cha weuo. Siku zile saba ziliposalia kidogo kutimia, Wayuda walitoka Asia wakamwona Paulo hapo Patakatifu, wakalichanganya kundi lote la watu, wakamkamata kwa mikono yao, wakapiga kelele kwamba: Waume na Isiraeli, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha po pote watu wote, waubeze ukoo wetu nayo Maonyo, hata mahali hapa! Tena ameingiza Wagriki hapa Patakatifu, ndivyo, alivyopapatia uchafu mahali hapa Patakatifu. Kwani kwanza walikuwa wamemwona mjini pamoja na Tirofimo wa Efeso, wakamwazia, ya kuwa Paulo amemwingiza napo Patakatifu. Mji wote ukatukutishwa, watu wote wakapakimbilia hapohapo, wakamkamata Paulo, wakamtoa hapo Patakatifu na kumburura; kisha milango yote ikafungwa papo hapo. Nao walipotaka kumwua, uvumi ulikuwa umemfikia mkuu wa kikosi cha askari, ya kuwa mji wote wa Yerusalemu umevurugika. Mara hiyo akachukua askari na wakubwa wao, akashuka kwao mbiombio. Wale walipomwona mkuu na askari, wakaacha kumpiga Paulo. Hapo, mkuu alipowafikia, akamshika, akaagiza, afungwe kwa minyororo miwili, akauliza: Nani huyu? Tena amefanya nini? Lakini watu kwa hivyo, walivyokuwa wengi, wengine wakapiga kelele hivyo, wengine hivyo. Asipoweza kuyatambua yaliyo kweli kwa ajili ya makelele akaagiza, apelekwe bomani. Alipofika pa kupandia akachukuliwa na askari, wamkingie ukorofi wa watu; kwani watu wengi mno walimfuata wakipiga kelele kwamba: Mwondoe huyu! Walipotaka kumwingiza bomani, Paulo akamwambia mkuu wa askari: Niko na ruhusa kukuambia neno? Naye aliposema: Unajua Kigriki? Wewe si yule Mmisri aliyefanya kishindo siku hizi akichukua watu 4000 waliokuwa wauaji na kuwapeleka nyikani? Paulo akasema: Mimi ni mtu wa Kiyuda toka mji wa Tarso, ni mwenyeji wa mji huo wa Kilikia usio mdogo; nakuomba, nipe ruhusa ya kusema na watu. Alipompa ruhusa, Paulo akasimama juu hapo pa kupandia, akawapungia watu mkono; nao walipokuwa kimya kabisa, akasema nao Kiebureo, akawaambia: Waume mlio ndugu na baba, sikilizeni, ninayojikania sasa mbele yenu! Waliposikia, ya kuwa anasema nao kwa msemo wao wa Kiebureo, wakakaza kunyamaza. Akasema: Mimi ni mtu wa Kiyuda, nimezaliwa Tarso katika nchi ya Kilikia. Nikalelewa humu mjini, nikakaa miguuni pa Gamalieli na kufundishwa Maonyo ya baba zetu kwa uangalifu wote. Nikajipingia kumfanyia Mungu kazi, kama nanyi nyote leo. Njia hiyo nikaifuata, mpaka nikiua watu; waume na wake nikawafunga na kuwatia kifungoni. Hayo hata mtambikaji mkuu na wazee wote watanishuhudia. Kisha nikapewa barua nao za kwenda kwa ndugu walioko Damasko, nako niwafunge wale waliokuwako, niwalete Yerusalemu, wapatilizwe. Lakini nilipokwenda na kufika karibu ya Damasko, ilipokuwa saa sita ya mchana, mara palitoka mwanga mkubwa mbinguni, ukanimulikia pande zote. Nikaanguka chini, nikasikia sauti iliyoniambia: Sauli, Sauli, unanifukuzaje? Nami nilipojibu: Ndiwe nani, Bwana? akaniambia: Mimi ni Yesu wa Nasareti, ambaye unanifukuza wewe. Nao wenzangu, tuliokuwa pamoja, waliuona mwanga, lakini aliyesema nami hawakumsikia sauti yake. Nilipouliza: Nifanyeje, Bwana? Bwana akanijibu: Inuka, uende Damasko! Ndimo, utakamoambiwa yote, uliyoagizwa kuyafanya. Kwa hivyo, nilivyokuwa sioni kwa kumetuka kwake ule mwanga, nikashikwa mkono na wenzangu, nikaingia Damasko. Kulikuwa na mtu, jina lake Anania, ni mwenye kuyashika Maonyo yote, kama wanavyomshuhudia Wayuda wote wanaokaa huko. Huyo akanijia, akasimama mbele yangu, akaniambia: Ndugu yangu Sauli, uwe mwenye kuona! Nami saa ileile nikapata kuona. Kisha akasema: Mungu wa baba zetu amekuchagua huko kale, upate kuyatambua, ayatakayo, umwone naye Mwongofu wake, uisikie na sauti ya kinywa chake mwenyewe, anavyokuambia: Utakuwa shahidi wangu kwa watu wote ukiwaambia, uliyoyaona nayo uliyoyasikia. Sasa unakawilia nini? Inuka, ubatizwe na kuoshwa, makosa yako yakuondoke, ukilitambikia Jina lake! Niliporudi Yerusalemu nikaja kuombea Patakatifu; hapo nikazimia roho, nikamwona, naye akaniambia; Piga mbio, utoke upesi Yerusalemu! Kwani hawatakupokea, ukinishuhudia mimi. Nam nikasema: Bwana, wao wenyewe wanajua, mimi nilivyowafunga waliokutegemea na kuwapiga mo mote nyumbani mwa kuombea. Napo hapo, damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama hapohapo kwa kupendezwa, nikayalinda mavazi yao wale waliomvua. Naye akaniambia: Enenda tu! Kwani mimi nitakutuma, uende mbali kwa wamizimu. Ndipo, wale waliomsikiliza mpaka neno hili walipopaza sauti wakisema: Mwondoe huyu nchini! Kwani haimpasi kuwapo. Walipopiga kelele hivyo na kuzirarua nguo zao na kutupa uvumbi juu angani, mkuu wa kikosi akaagiza, aingizwe bomani; akasema, wamwulize kwa mapigo, apate kuijua sababu ya kumpigia makelele kama hayo. Walipomfunga kwa mikanda, apigwe, Paulo akamwambia bwana askari aliyesimama hapo: Je? Mko na ruhusa kupiga mtu aliye Mroma, asipohukumiwa kwanza? Bwana askari alipovisikia hivi akamwendea mkuu wa kikosi, akamjulisha akisema: Wataka kufanya nini? Kwani mtu huyu ni Mroma. Mkuu wa kikosi akamwendea, akamwambia: Niambie, wewe u Mroma? Naye akasema: Ndio. Mkuu wa kikosi alipojibu: Mimi huu Uroma nimeununua kwa fedha nyingi, Paulo akasema: Mimi nimezaliwa nao. Papo hapo wale waliotaka kumwuliza kwa mapigo wakamwacha. Naye mkuu wa kikosi akaogopa alipotambua, ya kuwa ni Mroma, kwani yeye alimfunga. Kesho yake alitaka kuyatambua mashtaka ya Wayuda, kama ni ya kweli; kwa hiyo akamfungua, akaagiza, watambikaji wakuu na baraza yote ya wakuu wakusanyike pamoja, akampeleka Paulo chini kwao, akamsimamisha mbele yao. Paulo alipokwisha kuwakazia macho hao wakuu wa barazani, akasema: Waume ndugu, mimi mpaka siku hii ya leo nimekuwapo machoni pa Mungu, kwa hiyo moyo umening'aa wote. Mtambikaji mkuu Anania alipowaagiza waliosimama hapo, alipokuwa, wampige kinywani, ndipo, Paulo alipomwambia: Mungu atakupiga wewe, ukuta wenye uzuri wa kupakwa tu! Wewe unakaa kunihukumu, kama yanavyolingana na Maonyo, tena unayabeza Maonyo kwa kuagiza, nipigwe? Nao waliosimama hapo waliposema: Unamtukana mtambikaji mkuu wa Mungu? Paulo akasema: Ndugu zangu, sikumjua, ya kuwa ndiye mtambikaji mkuu, kwani imeandikwa: Mtawala ukoo wako usimwambia maovu! Paulo alipowatambua, ya kuwa fungu ni Masadukeo, fungu ni Mafariseo, akapaza sauti mbele yao wakuu: Waume ndugu, mimi ni Fariseo, mwana wa Fariseo: ninasutwa hivyo, tunavyoungojea ufufuko wa wafu. Aliposema hivi, Mafariseo na Msadukeo wakainukiana, nao wengi wakajitenga. Kwani Masadukeo hukana ya kwamba: Hakuna ufufuko, hakuna malaika, hakuna roho. Lakini Mafariseo huungama kwamba: Yote yapo. Yakawa makelele makubwa; palikuwa na waandishi waliokuwa wa upande wa Mafariseo, wakainuka, wakabishana wakisema: Mtu huyu hatumwoni kiovu cho chote. Kama yuko roho au malaika aliyesema naye, hatutaki kumgombeza Mungu. Lakini matata yalipokaza, mkuu wa kikosi akaogopa, Paulo asiraruliwe nao akaagiza, askari washuke, wampokonye katikati yao, wampeleke bomani. Usiku uliofuata Bwana akamjia na kusimama hapo, alipokuwa, akasema: Tulia! kwani kama ulivyoyashuhudia mambo yangu hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kuyashuhudia hata Roma. Kulipokucha, Wayuda wakakusanyika, wakaapizana, kwamba wasile, wala wasinywe, mpaka wamwue Paulo; nao walioapizana hivyo walikuwa wengi kupita 40. Kisha wakaendea watambikaji wakuu na wazee, wakasema: Tumeapizana kwa kiapo ya kwamba: Tusionje kitu, mpaka tumwue Paulo! Sasa ninyi wakuu nyote, mmweleze mkuu wa kikosi, amshushe kesho kwenu, kwamba mnataka kutambua kwa welekevu, mambo yake yalivyo. Lakini sisi tuko tayari kumwua, akiwa hajawafikia ninyi. Mwana wa umbu lake Paulo alipoisikia njama hiyo, akaja, akaingia bomani, akamjulisha Paulo. Ndipo, Paulo alipoita bwana askari mmoja, akasema: Umpeleke kijana huyu kwa mkuu wa kikosi! Kwani yuko na habari ya kumpasha. Yule akamchukua akampeleka kwa mkuu wa kikosi, akasema: Mfungwa Paulo umeniita, akataka, nimpeleke kijana huyu kwako, yuko na neno la kukuambia. Mkuu wa kikosi akamshika mkono, akaondoka naye kwenda penye njama, akamwuliza: Una habari gani ya kunipasha? Akasema: Wayuda wamepatana kukuomba wewe, umshushe Paulo kesho kwenye wakuu, kwamba wanataka kumwuliza kwa welekevu, mambo yake yalivyo. Basi, wewe usiwaitikie! Kwani watu wao wengi kupita 40 wanamwotea; hao wameapizana kwa kiapo, ya kwamba wasile, wala wasinywe, mpaka wamwue yeye. Sasa wako tayari na kuongoja, uwaitikie wewe. Mkuu wa kikosi akamwaga yule kijana, akamkataza kwamba: Usimwambie mtu, ya kuwa umenieleza haya! Akaita wabwana askari wawili, akasema: Tengenezeni askari 200, waende mpaka Kesaria, na askari wapanda frasi 70 na wenye mikuki 200, wawe tayari saa tatu ya usiku! Tandikeni na nyumbu za kumpandisha Paulo, wampeleke vema mpaka kwa Feliki aliye mtawala nchi! Akamwandikia barua yenye maneno haya: Mimi Klaudio Lisia nakuamkia wewe, mtawala nchi Feliki uliye na nguvu nyingi, salamu! Mtu huyu alikamatwa na Wayuda; nao walipotaka kumwua, nikaenda na kikosi cha askari, nikamwokoa, kwani nalisikia, ya kuwa ni Mroma. Nami kwa hivyo, nilivyotaka kutambua, waliyomsuta, nikamshusha na kumweka barazani kwao wakuu wao. Nikaona, ya kuwa anasutiwa mashindano ya Maonyo yao, lakini hakuna neno linalompasa kuuawa na kufungwa tu. Tena nilipoambiwa, ya kuwa mtu huyu anatunduiliwa, mara nikampeleka kwako, nikawaagiza hata wenye kumsuta, waseme mbele yako, wanayomsuta. Wale askari wakamchukua Paulo, kama walivyoagizwa, wakampeleka usiku mpaka mji wa Antipatiri. Kesho yake wakawaacha wale wapanda frasi, waondoke pamoja naye, nao wenyewe wakarudi bomani. Wale walipofika Kesaria wakampa mtawala nchi ile barua, wakamsimamisha Paulo mbele yake. Alipokwisha kuisoma hiyo barua, akamwuliza upande wa nchi, aliotoka. Aliposikia, ya kuwa ni mtu wa Kilikia, akasema: Nitakuuliza na kukusikiliza, wewe kukusuta watakapofika; kisha akaagiza, alindwe katika boma la Herode. Siku tano zilipopita, mtambikaji mkuu Anania akatelemka pamoja nao wazee wengine na msemaji aliyitwa Tertulo, wakamsuta Paulo mbele ya mtawala nchi. Yule alipoitwa, Tertulo akaanza kumsuta akisema: Kwa nguvu yako, bwana Feliki, tunapata kutengemana sana; na kwa utunzaji wako wewe hili taifa letu limetengenezewa mambo mazuri mengi. Hayo yote twayapokea na kukushukuru sana kila siku na kila mahali. Lakini nisikuchokeshe kwa maneno mengi; nakuomba utusikilize kidogo kwa utu wako. Kwani tumemwona mtu huyu kuwa mwangamizi, akiwaletea kondo Wayuda wote waliopo ulimwenguni po pote, tena ni mkubwa wa chama cha Wanasareti. Alipojaribu kupachafua napo Patakatifu, ndipo, tulipomkamata tukitaka kumhukumu kwa Maonyo yetu. Lakini mkuu wa kikosi Lisia akamwondoa na nguvu nyingi mikononi mwetu, akaagiza, wenye kumsuta waende kwako wewe. Hayo yote, tunayomsuta, utaweza kuyatambua mwenyewe ukimwulizauliza. Wayuda nao wakamwitikia wakisema: Hivyo ndivyo, yalivyo. Mtawala nchi alipomkonyeza Paulo, aseme, akajibu: Ninakujua, ya kuwa wewe ndiwe mwamuzi wa hili taifa letu tangu miaka mingi; kwa hiyo nitajikania haya mambo yangu na kuchangamka. Kwani wewe unaweza kutambua, ya kuwa siku, nilizopanda kwenda Yerusalemu kuombea hapo, hazijapita kumi na mbili. Tena hawakuniona hapo Patakatifu, nikiongea na mtu au nikiwachokoza watu, wainukiane, kama ni nyumbani mwa kuombea au mjini pengine. Tena wanayonisuta sasa, hawawezi kuyatokeza kuwa ya kweli mbele yako. Lakini mbele yako naungama waziwazi: Njia ile, wanayoiita ya chama, ndiyo yangu ya kumtumikia Mungu wa baba zetu, nikayategemea yote yaliyoandikwa penye Maonyo na katika vyuo vya Wafumbuaji. Tena liko jambo, ninalolingojea kwa Mungu, nalo ndilo, wanaloliitikia nao hawa wenyewe, la kwamba: Utakuwapo ufufuko wa waongofu na wa wapotovu. Kwa hiyo nami mwenyewe nakaza kuulinda moyo wangu, uwe umeng'aa mbele ya Mungu, hata mbele ya watu katika mambo yote. Mika ilipopita mingi, nikafika kwao wa taifa langu niwapelekee sadaka ya vipaji. Hapo ndipo, waliponiona, nikieuliwa Patakatifu; hawakuniona, nikikusanya watu au nikipiga kelele. Lakini walioniona ndio Wayuda wengine waliotoka Asia; hao ingewapasa kuwapo hapa, wanisute mbele yako, waliyonionea. Nao hawa na waseme wenyewe, kama wameona upotovu kwangu, niliposimama mbele yao wakuu, lisipokuwa neno lile moja, nililolipazia sauti kabisa nikiinuka katikati yao na kusema: Ufufuko wa wafu ndio, ninaohukumiwa leo mbele yenu! Feliki alipoyasikia haya akawakawilisha, kwani alipata kuelewa na mambo ya njia hiyo. Kwa hiyo akasema: Mkuu wa kikosi Lisia atakapotelemka, nitayatambulisha naye mambo yenu. Akamwagiza bwana askari, Paulo alindwe, lakini asifungwe, wala asiwazuie wenziwe kumtumikia au kumjia. Siku zilipopita, Feliki akaja pamoja na mkewe Dirusila aliyekuwa Myuda, akatuma kumwita Paulo, akamsikiliza, akimwonyesha, kumtegemea Kristo Yesu kulivyo. Lakini alipoeleza mambo ya kupata wongofu na ya kuziepuka tamaa na ya hukumu itakayokuwapo, Feliki akaingiwa na woga, akajibu: Sasa hivi jiendee tu! Hapo, nitakapopata mapumziko, nitakuita tena. Vile vile alingojea kupenyezewa fedha na Paulo, amfungue. Kwa hiyo akamwita mara kwa mara, aongee naye. Lakini miaka miwili ilipopita, Porkio Festo akampokea Feliki kazi yake. Feliki akataka kuwapendelea Wayuda, kwa hiyo akamwacha Paulo kifungoni. Festo alipokwisha kuupata utawala nchi, siku zilipopita tatu, akaondoka Kesaria, akapanda kwenda Yerusalemu. Ndipo, watambikaji wakuu na Wayuda wenye cheo walipomtokea kumsuta Paulo, wakambembeleza na kumwomba, awapendeze akiagiza, aletwe Yerusalemu, kwani walikwisha kula njama ya kumwua njiani. Festo akajibu: Paulo analindwa huko Kesaria, nami mwenyewe nitaondoka upesi kwenda huko. Kisha akasema: Wenzenu wanaoweza wafuatane nami, wamsute huko mtu huyo, akiwa ametenda neno lisilopasa! Alipokwisha kukaa kwao siku zisizopita nane au kumi, akatelemka kwenda Kesaria. Kesho yake akaketi katika kiti cha uamuzi, akaagiza, Paulo aletwe. Alipofika, Wayuda waliotelemka toka Yerusalemu wakamsimamia pande zote, wakamsingizia mambo mengi yaliyokuwa magumu, wasiweze kuyaonyesha kuwa ya kweli. Lakini Paulo akajikania akisema: Sikukosa wala Maonyo ya Wayuda, wala Patakatifu, wala Kaisari. Kwa kutaka kuwapendeza Wayuda Festo akamwuliza Paulo akisema: Unataka kupanda kwenda Yerusalemu, uhukumiwe huko mbele yangu kwa ajili ya mambo hayo? Paulo akasema: Ninasimama hapa penye kiti cha uamuzi cha Kaisari; ndipo panaponipasa kuhukumiwa. Wayuda hakuna, nilichowapotolea, kama nawe mwenyewe unavyojua. Basi, nikiwa mpotovu, nikatenda linalopasa kuuawa, sikatai kufa. Lakini masingizio yao hawa yakiwa hayana maana, hakuna tena anayeweza kunitia mikononi mwao, kwamba awapendeze. Nataka, nihukumiwe na Kaisari. Hapo Festo akasemezana nao wakuu, akajibu: Umetaka kuhukumiwa na Kaisari, utakwenda kwake Kaisari. Siku zilipopita, mfalme Agripa na Berenike wakafika Kesaria, wamwamkie Festo. Walipokaa huko siku nyingi, Festo akamwelezea mfalme mambo ya Paulo akisema: Yuko mtu aliyeachwa na Feliki kifungoni. Nilipokuwa Yerusalemu, watambikaji wakuu na wazee wa Wayuda walinitokea kwa ajili yake, wakataka mapatilizo yake yeye. Nikawajibu: Si desturi ya Kiroma kutoa mtu ye yote kwa mapenzi ya wengine; sharti kwanza mwenye kusutwa aonane uso kwa uso nao wasutaji wake, naye apate pa kujikania alilosutwa. Basi, walipokusanyika huku, sikuwakawilisha, ila kesho yake nikaketi katika kiti cha uamuzi, nikaagiza, yule mtu aletwe. Wasutaji walipomwinukia, vibaya nilivyoviwaza moyoni, hakuna, walichomsingizia hata kimoja; wakabishana naye tu kwa ajili ya tambiko lao wenyewe na kwa ajili ya mfu anayeitwa Yesu, kwani Paulo alisema: Yupo, anaishi. Nami kwa hivyo, nisivyojua mabishano kama hayo, nikamwuliza: Unataka kwenda Yerusalemu, uhukumiwe huko mambo hayo? Lakini Paulo akasema waziwazi, ya kuwa anataka kuwekwa, mpaka ahukumiwe na mfalme aliye mkuu peke yake; kwa hiyo nikaagiza, awekwe, mpaka nitakapomtuma kwake Kaisari. Agripa alipomwambia Festo: Nami mwenyewe nataka kumsikia mtu huyu akasema: Kesho utamsikia. Basi, kesho yake wakaja Agripa na Berenike, walikuwa wamejipamba kifalme vizuri, wakaingia penye hukumu pamoja na mabwana wakubwa na watu wenye cheo wa mjini. Festo alipoagiza, Paulo akaletwa. Ndipo, Festo aliposema: Mfalme Agripa, nanyi waume nyote mliopo hapa pamoja nasi, mtazameni mtu huyu! Kwa ajili yake yeye kundi lote zima la Wayuda limenitokea huko Yerusalemu na hapa vilevile; wakanipigia makelele ya kwamba: Haifai kabisa, huyu akiwapo vivyo hivyo! Lakini mimi nikaona, ya kuwa hakufanya neno lo lote linalopasa, auawe, naye mwenyewe akasema waziwazi: Nataka, nihukumiwe na mfalme aliye mkuu peke yake; kwa hiyo nikataka kumtuma huko. Lakini sinalo neno la kweli la kumwandikia bwana wangu la kwamba: Amekosa hivi na hivi. Kwa hiyo nimemleta mbele yenu, kwanza mbele yako wewe, mfalme Agripa, nipate la kuandika, mkiisha kuulizana naye. Kwani naona, ni upambavu kutuma mfungwa, pasipo kuyaeleza makosa yake. Agripa alipomwambia Paulo: Una ruhusa kujisemea mwenyewe, ndipo, Paulo aliponyosha mkono, akajikania hivyo: Mfalme Agripa, ninashangilia moyoni, kwa kuwa yote, ninayosutwa na Wayuda, nitajikania leo mbele yako wewe, uliyeyatambua sanasana mazoea na mashindano yote ya Kiyuda. Kwa hiyo nakuomba, unisikilize kwa kuvumilia. Mwendo wangu ulivyokuwa hapo mwanzo, nilipokuwa kijana pamoja na vijana wenzangu huko Yerusalemu, Wayuda wote wanavijua. Kwani wamenitambua kale; wakitaka wangenishuhudia, ya kwamba nimekifuata kile chama kinachokaza kuyashika mambo ya tambiko letu, kwani nalikuwa Fariseo. Hata sasa ninasimama hapa, nihukumiwe, kwa sababu nangojea, kile kiagio kitimie, Mungu alichokiagana na baba zetu. Vile vile mashina yetu kumi na mawili hungojea, wakifikie; kwa hivyo wanajihimiza kumtumikia Mungu usiku na mchana. Hicho kingojeo ndicho, ninachosutiwa na Wayuda, mfalme Agripa. Kwa sababu gani huwaza kwenu, ya kuwa neno hilo halitegemeki la kwamba: Mungu anafufua wafu? Kweli nami vyaliniingia moyoni kwamba: Sharti nifanye mdngi ya kulipinga Jina la Yesu wa Nasareti. Hayo niliyafanya huko Yerusalemu; nilipopewa ruhusa na watambikaji wakuu nikawatia watakatifu wengi kifungoni, tena walipouawa, nami nikasaidia. Hata katika nyumba zote za kuombea niliwaumiza mara kwa mara, nikiwashurutisha kumbeza Yesu, nikawaendea na ukorofi kama mwenye wazimu, nikawakimbiza mpaka kwenye miji iliyoko ugenini. Kwa hiyo nikaenda hata Damasko, nilipokwisha kupata maelekezo na maagizo kwa watambikaji wakuu. Ilipokuwa saa sita ya mchana, ndipo, mfalme, nilipoona hapo njiani mwanga uliotoka mbinguni wenye kumetuka kulishinda jua, ukatumulikia pande zote mimi na wenzangu waliokwenda pamoja nami. Tulipoanguka chini sote, nikasikia sauti iliyoniambia kwa msemo wa Kiebureo: Sauli, Sauli, unanifukuzaje? Utashindwa na kupiga mateke penye machomeo. Mimi nilipouliza: Ndiwe nani, Bwana? Bwana akasema: Mimi ni Yesu, ambaye unanifukuza wewe. Lakini inuka, usimame kwa miguu yako! Kwani hii ndiyo, niliyokutokea; Nikulinganye, utumike kuyashuhudia, uliyoyaona, nayo utakayoonyeshwa nami. Nitakuokoa kwao walio wa kwenu nako kwao wamizimu, maana ndiko, nitakakokutuma, uwafumbue macho yao na kuwaongoza, watoke gizani, waingie mwangani, tena watoke katika nguvu ya Satani, wamfikie Mungu; hivyo watapata kuondolewa makosa na kupewa fungu lao penye watakatifu, wakiwa wakinitegemea. Hapo, mfalme Agripa, sikukataa kuliitikia hilo jambo la mbinguni, nililoliona, ila niliwatumikia kwanza wa Damasko, tena wa Yerusalemu, tena wote walioko katika nchi ya Yudea, kisha hata wamizimu nao, nikiwaambia, wajute wakimgeukia Mungu na kutenda matendo yaliyo ya kujuta kweli. Kwa sababu hiyo Wayuda walinikamata, nilipokuwa hapo Patakatifu, wakajaribu kuniua. Lakini kwa hivyo, nilivyopata msaada kwa Mungu, ninasimama mpaka siku hii ya leo nikiwaeleza wakubwa na wadogo; sisemi mengine, yasipokuwa yale, waliyoyasema Wafumbuaji na Mose kwamba: Yatakayokuwapo ni haya: Kristo sharti ateswe, kisha atakuwa limbuko la ufufuko wa wafu, kisha atawaalika wao wa ukoo huu nao wamizimu, wafike mwangani. Alipojikania hivyo, Festo akapaza sauti akisema: Paulo, una wazimu! Ujuzi wako mwingi unakupapayusha. Paulo akasema: Bwana wangu Festo, sina wazimu, ila natoa maneno yenye kweli na yenye maana. Nawe mfalme, haya unayajua vema; kwa hiyo nasema mbele yako waziwazi. Kwani najua sana, ya kuwa hayo yote hakuna hata moja, usilolitambua, kwa sababu hayo hayakufanyika pembeni. Mfalme Agripa, unawategemea Wafumbuaji? Nimekujua, ya kuwa unawategemea. Agripa akamwambia Paulo: Pamesalia padogo, ungenishinda, nikawa Mkristo. Ndipo, Paulo aliposema: Namwomba Mungu, paliposalia padogo napo paliposalia pakubwa, wote hapa walionisikia leo, si wewe tu, awape kuwa, kama mimi nilivyo, pasipo minyororo hii. Kisha mfalme na mtawala nchi na Berenike nao waliokaa pamoja nao wakainuka, wakajongea pembeni, wakasemezana wao kwa wao: Mtu huyu hakufanya neno linalopasa, auawe au afungwe. Agripa akamwambia Festo: Mtu huyu angeweza kufunguliwa, kama asingalikuwa ametaka kuhukumiwa na Kaisari. Mambo yalipokatwa, kwamba tutweke kwenda Italia, wakamtia Paulo na wafungwa wengine mikononi mwa bwana askari, jina lake Yulio aliyekuwa wa kikosi kilichomlinda mfalme aliye mkuu peke yake. Tukaingia chomboni kilichotoka Adaramiti, kilichotaka kwenda katika miji ya Asia, tukaondoka. Tukawa na Aristarko wa Tesalonike wa Makedonia. Kesho yake tukafikia Sidoni; Yulio aliyemtunza Paulo kwa upole akampa ruhusa kwenda kwa rafiki zake, apate kugawiwa nao pamba za njiani. Tulipotweka huko tukakielekeza chombo kwenda kandokando ya Kipuro, kwa sababu pepo zilitujia mbele. Tulipokwisha kuivuka bahari ya Kilikia na ya Pamfilia, tukafika Mira wa Likia. Huku bwana askari akaona chombo kilichotoka Alekisandria kwenda Italia, akatupakia mle. Lakini siku nyingi tukasumbuka sana kukiendesha kidogo tu, tupate kufika upande wa Kinido, kwani upepo ulituzuia. Tukapita kandokando ya Kreta upande wa Salmone. Hapo ikawa kazi kubwa kukielekeza chombo baharini, kisha tukafika mahali panapoitwa Matuo Mazuri, ni karibu ya mji wa Lasea. Hivyo siku zilizopita zikawa nyingi, tena kwenda baharini siku zile kukaponza watu wana, kwa sababu hata siku za kufunga zilikuwa zimepita. Paulo akawaonya akiwaambia: Waume wenzangu, naona, ya kuwa mwendo wa sasa utakuwa wa maumivu, tena vitakavyopotea ni vingi, si mizigo tu na chombo, ila na sisi wenyewe. Lakini bwana askari akamsikiliza mwelekeze chombo na mwenye chombo, asiyafuate yaliyosemwa na Paulo. Kwa sababu kituo hakikufaa vema kukaa huko siku za kipupwe, walio wengi walitaka kabisa kuondoka huko, wajisumbuesumbue kukifikisha chombo Foniki, wakae huko siku za kipupwe, kwani ilikuwa bandari ya Kreta iliyokinga pepo za machweoni kwa jua upande wa kusini na wa kaskazini. Upepo wa kusini ulipoanza kuvuma, wakawaza, ya kuwa wamavipata, walivyovitaka, wakang'oa nanga, wakaendelea kandokando ya pwani pa Kreta. Lakini kitambo kidogo kilipopita, wakatokewa na upepo mkali wenye ngurumo unaoitwa kwao Mkweza Mawimbi. Chombo kikapokonywa nao, kisiweze kuushinda upepo huo na kuuelekea, kwa hiyo tukakiacha, kichukuliwe nao. Tukaenenda na kukimbizwa na upepo, tukafika kwenye kisiwa kidogo, jina lake Klauda, hapo tukakaza nguvu zote, tupate kuipandisha mashua; palisalia kidogo tu, tungeshindwa. Lakini walipokwisha kuipandisha wakaitumia, iwasaidie; wakaifunga chomboni na kuikinga, wakapitisha kamba hata chini. Tena woga ukawaingia wa kutumbukia panapoitwa Sirti, kwa hiyo wakalishusha tanga, chombo kikaendeshwa hivyo. Kesho yake upepo ukizidi kutuvumia kwa nguvu zote, wakatupa mizigo baharini. Siku ya tatu tukatupa kwa mikono yetu hata vitu vya chombo. Lakinia zilipokuwa siku nyingi, lisituonekee wala jua wala nyota, upepo ukikaza vivyo hivyo, basi, mwisho hakuwako tena mwenye moyo wa kwamba: Tutaokoka. Walipoacha kula vyakula siku nyingi, ndipo, Paulo alipoinuka katikati yao, akasema: Waume wenzangu, kama mngalilifuata neno langu, mkaacha kuondoka huko Kreta, hatungaliyapata maumivu na mapotevu haya. Lakini na sasa nawaonya, mtulie mioyo; kwani miongoni mwenu ninyi hamna atakayeangamia hata mmoja, kisipokuwa chombo hiki tu. Kwani malaika wa Mungu wangu, ninayemtumikia, amesimama usiku huu hapo, nilipo, akasema: Usiogope, Paulo, wewe sharti usimame mbele ya Kaisari! Tena tazama, Mungu amekupa wote waliomo humu chomboni pamoja nawe. Kwa hiyo tulieni mioyo, waume wenzangu! Kwani namtegemea Mungu, ya kwamba: Itakuwapo vivyo hivyo, kama nilivyoambiwa. Lakini sharti tupwelewe kisiwani kulikokuwa kote. Usiku wa kumi na nne ulipofika, nasi tulipotupwa huko na huko katika bahari ya Adiria, usiku wa manene wabaharia wakawaza kwamba: Nchi iko karibu. Walipokishusha kipimo, wakapaona, pana mikono 60. Walipoendelea kidogo, wakakishusha kipimo tena, wakapaona, pana mikono 45. Tukaogopa, tusitupwe mahali penye miamba, kwa hiyo wakatia nanga nne za nyuma, wakangoja, kuche. Lakini wabaharia walitaka kukimbia na kukiacha chombo. Kwa hiyo wakaishusha mashua baharini, wakasema: Twataka kuzitia hata nanga za mbele. Ndipo, Paulo alipomwambia bwana askari nao askari wenyewe: Hawa wasipokaa humu chomboni, ninyi hamtaweza kuokoka. Ndipo, askari walipozikata kamba za masha, wakaiacha, ianguke baharini. Kulipopambazuka, Paulo akawabembeleza wote, wale chakula, akisema: Leo ni siku ya kumi na nne, mkikaa kwa kungoja na kufunga; hakuna kitu cho chote, mlichokitia vinywani. Kwa hiyo nawabembeleza, mle chakula, kwani hiki kitaufalia wokovu wenu. Kwani kwenu hakuna hata mmoja atakayeangamiza hata unywele mmoja tu wa kichwani. Naye alipokwisha kuyasema haya, akachukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega, akaanza kula. Ndipo, wote walipotulia mioyo, wakala chakula nao. Nasi sote tuliokuwa humo chomboni wote pamoja tulikuwa watu 276. Waliposhiba vyakula wakaupunguza uzito wa chomboni wakitupa ngano baharini. Kulipokucha, hawakuitambua nchi. Lakini walipoona kituo penye ufuko, wakataka kukiingiza chombo huko, ikiwezekana. Wakazikata kamba za nanga, wakaziacha baharini; hapohapo wakazilegeza nazo kamba zilizofunga sukani, wakatweka tanga dogo na kulielekezea upepo, wakaufuata ufuko. Lakini tulitupwa funguni, chombo kikakwama mbele, kikachimba mchangani, kikashikwa kabisa, kisitukutike hata kidogo, lakini nyuma kikavunjwa kwa nguvu ya mawimbi. Askari walipotaka kuwaua wafungwa, maana mtu asipate kukimbia kwa kuogelea, bwana askari alitaka kumwokoa Paulo, akawazuia, wasivifanye, walivyovitaka; kisha akawaagiza wanaojua kuogelea, wajitupe wa kwanza baharini, wafike pwani. Waliosalia waliambiwa, wajiokoe na kutumia mbao au miti minginemingine ya chomboni. Hivyo wote wakapata kuokoka na kufika salama penye nchi kavu. Tulipokwisha kuokoka, ndipo, tulipoambiwa, ya kuwa kisiwa kinaitwa Melite. Wenyeji wa huko wakatutunza kwa upendo usiopatikana kila siku: wakawasha moto, wakatupokea mwao sisi sote kwa ajili ya mvua iliyotunyea na kwa ajili ya baridi. Paulo alipodondoa mzigo wa vijiti kuvitia motoni, mkatoka humo nyoka kwa ajili ya moto, akamzingazinga mkono. Wenyeji walipomwona yule mdudu, alivyomng'ang'ania mkononi pake, wakasemezana wao kwa wao: Mtu huyu hakosi kuwa mwuaji, kwani ingawa ameokoka baharini, tena lipizi halimwachi, awepo. Alipomkung'uta yule mdudu motoni, hakuna kiovu tena kilichompata. Lakini wale walimtunduia na kungoja, avimbe au aanguke chini akifa papo hapo. Lakini walipongoja sana na kuona, ya kuwa hapati kibaya cho chote, wakageuka na kusema: Yeye ni mungu! Lakini hapo karibu palikuwa na kiunga cha mkuu wa kisiwa, jina lake Pubulio. Huyu akatupokea mwake siku tatu, akatutunza na kutupendeza. Baba yake Pubulio alipoingiwa na homa na kuhara damu, Paulo akaingia mwake, akamwombea, akambandikia mikono, akamponya. Hayo yalipokwisha kufanyika, nao wengine wa kisiwa kile waliokuwa wenye magonjwa wakamjia, wakaponywa, wakatutukuza kwa matukuzo mengi. Nasi tulipoingia chomboni tena, wakatupakilia navyo vyote vya kutumia njiani. Miezi mitatu ilipopita, tukaondoka tukijipakia chomboni kilichotoka Alekisandria; kilikuwa kimezimaliza siku za kipupwe pale kisiwani; kilikuwa chenye chapa cha mapacha. Tulipofika Sirakuse, tukakaa huko siku tatu. Kutoka huko tukazunguka, tukafika Regio. Tulipongoja siku moja, kukavuma upepo wa kusini, tukafika Puteoli kwa mwendo wa siku mbili. Huko tukakuta ndugu, tukabembelezwa nao, tukae kwao siku saba. Ndivyo, tulivyokwenda kufika Roma. Ndugu wa huko walipovisikia wakaja kukutana na sisi, wakatujia mpaka Apioforo, wengine mpaka Tiretaberne. Paulo alipowaona akamshukuru Mungu, akachangamka. Tulipoingia Roma, bwana askari akampa mwenzake mkubwa wafungwa, lakini Paulo akapewa ruhusa ya kukaa, alipotaka, pamoja na askari aliyemlinda. Siku tatu zilipopita, akawakusanya wakubwa wa Wayuda. Walipokusanyika, akawaambia: Waume ndugu, mimi sikuwakosea wao wa ukoo wetu wala mazoea ya baba zetu. Nimefungwa huko Yerusalemu, nikatiwa mikononi mwa Waroma. Nao waliponiulizauliza wakataka kunifungua, kwa sababu kwangu hakuna neno linalopasa, niuawe. Lakini Wayuda walipobisha, nikashurutishwa kutaka kuhukumiwa na Kaisari, lakini hapo siko kwamba: Niwasute walio wa taifa langu. Kwa sababu hii nimewaita, niwaone ninyi, tusemeane. Kwani kingojeo cha Waisiraeli ndicho, nilichofungiwa mnyororo huu. Nao wakamwambia: Sisi kwa ajili yako hatukupata barua toka Yudea, wala hakuna ndugu aliyetujia na kutusimulia mambo yako, wala kusema kibaya, ulichokifanya. Lakini twataka kusikia kwako mwenyewe mawazo yako, kwani chama hiki tumekijua, nako kwetu kinatambulika, ya kuwa kinabishiwa po pote. Walipokwisha kuagana naye siku, wengi wakamjia huko, alikofikia, akawaeleza tangu asubuhi mpaka jioni akiushuhudia ufalme wa Mungu; tena akajaribu kuwashinda kwa ajili yake Yesu na kuwafumbulia maonyo ya Mose na maneno ya wafumbuaji wengine wakayaitikia maneno yake, wengine wakakataa kuyategemea. Wengine wakayaitikia maneno yake, wengine wakakataa kuyategemea. Hivyo wakashindwa kupatana wao kwa wao, wakajiendea zao. Ndipo, Paulo aliposema neno kwa kinywa cha mfumbuaji Yesaya: Nenda kwao wa ukoo huu, useme: Kusikia mtasikia, lakini hamtajua maana; Kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Kwani mioyo yao walio ukoo huu imeshupazwa, wasisikie kwa masikio yao yaliyo mazito, nayo macho yao wameyasinziza, wasije wakaona kwa macho yao, au wakasikia kwa masikio yao, au wakajua maana kwa mioyo yao, wakanigeukia, nikawaponya. Basi, ijulikane kwenu ninyi ya kwamba: Wokovu huu wa Mungu umepelekwa kwenye wamizimu; hao ndio watakaousikia. Alipovisema hivyo, Wayuda walikwenda wakibishana sana wao kwa wao. Paulo akakaa miaka miwili mzima katika nyumba yake, aliyokuwa ameipanga, akawapokea wote walioingia kwake, akautangaza ufalme wa Mungu, akayafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo pasipo woga na pasipo kuzuiliwa na mtu. Mimi Paulo nilye mtumwa wa Kristo Yesu nimeitwa kuwa mtume kwa hivyo, nilivyochaguliwa, niutangaze Utume mwema wa Mungu. Huo aliuagia kale kwa vinywa vya Wafumbuaji wake waliouandika katika barua takatifu; ni mambo ya Mwana wake Yesu Kristo, Bwana wetu. Huyu alizaliwa kimtu katika uzao wa Dawidi, tena hapo, alipofufuliwa katika wafu, ikatokea waziwazi, ya kuwa ni Mwana wa Mungu kwa nguvu ya Kiroho iliyo yenye kutakasa. Yeye ndiye aliyetugawia kuwa mitume, tuwafundishe wamizimu wote usikivu wa kumtegemea, Jina lake litukuzwe. Miongoni mwao mlikuwa nanyi, mkaitwa na Yesu Kristo. Nawaandikia nyote mnaokaa Roma, mlio wapenzi wa Mungu, mlioitwa kuwa watakatifu: Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo! Kwanza ninamshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu ninyi nyote, kwa kuwa hivyo, mnavyomtegemea, hutangazwa ulimwenguni mote. Kwani Mungu, ninayemtumikia moyoni mwangu kwa kuutangaza Utume mwema wa Mwana wake, huyu Mungu ni shahidi wangu, ya kuwa sikuacha kuwakumbuka ninyi siku zote po pote, ninapoomba. Ninalojiombea ni hili: Mungu apendezwe kunifungulia ile njia nzuri ya kuja kwenu, kwani ninatunukia kuonana nanyi, nipate kuwagawia nanyi kipaji chochote cha Kiroho, mshupazwe vizuri. Hivyo tutatulizana mioyo pamoja nanyi na kuonyeshana mategemeo yetu, tunayoyakalia ninyi na mimi. *Lakini ndugu zangu, sitaki, mkose kujua, ya kuwa nilijielekeza mara nyingi, nije kwenu, nione pato hata kwenu, kama nilivyoliona kwa wamizimu wengine; lakini nimezuiliwa mpaka leo hivi. Nimeingia udeni kwa Wagriki hata kwa washenzi, kwa wajuzi hata kwa wapuzi. Kwa hivyo, nilivyo mimi, nimekwisha kujifunga, niwapigie nanyi ile mbiu njema huko Roma. Maana sioni soni ya kuutangaza Utume mwema wa Kristo, kwani unayo nguvu ya Mungu ya kuwaokoa wo wote wanaoutegemea, kwanza Wayuda, kisha Wagriki nao. Kwani humo unafunuliwa wongufu wa Kimungu, wanaopewa wenye kumtegemea, wajikaze kumtegemea. Ndivyo vilivyoandikwa ya kuwa: Mwongofu atapata uzima kwa kumtegemea Mungu. Kwani makali ya Mungu yanashuka toka mbinguni, yawatokee watu wote wasiomcha Mungu nao wenye upotovu, wanaoyazuia yaliyo ya kweli kwa upotovu wao; kwani mambo ya Mungu yametambulikana kwao, maana yalifumbuliwa, naye Mungu ndiye aliyewafumbulia. Kwani hivyo, ambavyo macho ya watu hayajaviona, maana nguvu yake ya kale na kale na Kimungu chake, hujulikana, tena huonekana, mtu akivitazama, Yeye alivyovifanya tangu hapo, alipouumba ulimwengu; kwa hiyo hawana la kujikania.* Wangawa walimtambua Mungu, hawakumtukuza kwamba: Ni Mungu, wala hawakumshukuru, Kwa hiyo mawazo yao yakawa ya bure, nayo mioyo yao isiyoyajua yaliyo ya kweli ikaingiwa na giza. Walipojiwazia kuwa werevu wa kweli, ndipo, walipopumbazika. Wakaugeuza utukufu wa Mungu asiyeoza, wakamfananisha na mfano wa sura ya mtu anayeoza na wa ndege na wa nyama na wa wadudu. Kwa hiyo Mungu akawatupa, wajichafue wakizifuata tamaa za mioyo yao na kujipujua, mpaka wakifujiana miili yao wao kwa wao; ni wao hao walioigeuza kweli ya Mungu kuwa uwongo, wakakitambikia kiumbe na kukitumikia kuliko Muumbaji aliye mwenye kutukuzwa kale na kale. Amin. Kwa hiyo Mungu aliwatupa, waingiwe na tamaa za upujufu. Kwani hata wanawake wao wakayageuza matumikio yao ya kimtu, wakazusha mengine yasiyo ya kimtu. Vile vile hata waume wakaacha kuwatumia wanawake kimtu, tena kwa hivyo, tamaa zao zilivyowachoma kama moto, wakatumiana waume na waume wenzao; wakafanya hayo yasiyopasa kamwe, wakapata malipo ya upotevu wao yaliyowapasa. Tena kwa hivyo, walivyokataa kumshika Mungu na kumtambua, Mungu aliwatupa, wafuate mawazo ya ujinga na kufanya yasiyompasa mtu. Wakaenea upotovu wote na ubaya na choyo na uovu, wakajaa kijicho na uuaji na magombano na manyatio na mazoezo maovu. Ndio watetaji, wabishi, wasingiziaji, wenye kumbeza Mungu na kubeza watu, wenye kujivuna na kujitukuza, wenye maoneo maovu na wenye kuwakataa wazee. Hawana utambuzi wala welekevu wala upendo wala huruma. Nao walikuwa wameyambua yaliyoongoka mbele ya Mungu kwamba: Wanaoyatenda mambo hayo wamepaswa na kuuawa; tena hawayafanyi tu hayo, lakini nao wengine wakiyatenda, wanapendezwa. *Kwa hiyo huna la kujikania, wewe uwaye yote, ukiumbua wengine. Kwani kwa hilo, unalomwumbua mwingine, unajionea patilizo mwenyewe. Kwani wewe muumbuaji unayafanya yayo hayo. Nasi twajua, ya kuwa wenye mambo kama hayo Mungu hwaumbua kweli, wajulike, walivyo. Lakini wewe ukiumbua wengine walio wenye mambo unayoyafanya, kisha unayafanya yaleyale, unajiwaziaje, ya kwamba wewe utaipona hukumu ya Mungu? Au unaubeza wema na uvumilivu na ungojevu wake mwingi? Hujui, ya kuwa wema wa Mungu unakuonyesha njia ya kujuta? Lakini wewe mwenye moyo mgumu unaokataa kujuta unajilimbikia mwenyewe makali, yakupate siku ya makali, hukumu inayopasa itakapofunuliwa na Mungu. Ndipo, atakapomlipa kila mtu, kama matendo yake yalivyo: wale wasiochoka kufanya mema kwa kutafuta utukufu na heshima na mengine yasiyooza, hao watapewa uzima wa kale na kale. Lakini wale wachokozi wanaokataa kuyatii yaliyo ya kweli kwa kupendezwa na upotovu, hao watapata makali yenye moto. Maumivu na masongano yataupata moyo wa kila mtu anayefanya maovu, kwanza Wayuda, kisha Wagriki nao. Lakini utukufu na heshima na utengemano ndio, atakaoupata kila anayefanya mema, kwanza Wayuda, kisha Wagriki nao. Kwani Mungu hautazami uso wa mtu.* Kwani wote waliokosa wasipoyajua Maonyo huangamia tu pasipo Maonyo, nao wote waliokosa wakiyajua Maonyo hao watahukumiwa kwa Maonyo. Kwani walio wenye wongofu machoni pa Mungu sio wenye kuyasikia Maonyo, ila wenye kuyafanya Maonyo ndio watakaopewa wongofu. Kwani wamizimu wasiopata maonyo wakiyafanya mambo ya Maonyo wenyewe, basi, hao wasiopata maonyo mioyo yao ndiyo iliyokuwa maonyo yao. Hao wanaonyesha, ya kuwa kazi, Maonyo yanayoitaka, imeandikwa mioyoni mwao; nayo, wanayoyajua mioyoni, huwashuhudia, ndiyo mawazo ya mioyo yanayoinukiana, nayo mengine yanayokaniana. Haya yatajulikana siku ile, Mungu atakapompa Kristo Yesu kuyaumbua yaliyofichwa na watu. Huu ndio Utume mwema, niliopewa. Angalia, wewe unayeitwa Myuda, unayatumia Maonyo ya kupumzikia ukijivunia kwamba: Mungu ninaye! Kweli unayatambua, anayoyataka, kisha ukayatenga yaliyo mepesi nayo yaliyo magumu, kwa kuwa umefundishwa mambo ya Maonyo. Hivyo unajiwazia mwenyewe kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga wao wakaao gizani, ukataka kuonya wajinga na kufundisha wachanga, kwani Maonyo yalikuwa yamekuonyesha, jinsi mtu anavyopata utambuzi na ukweli. Je? Wewe unayefundisha mwingine, hujifundishi mwenyewe? Je? Wewe unayetangaza, wasiibe, huibi mwenyewe? Je? Wewe unayesema, wasizini, huzini mwenyewe? Je? Wewe unayechukizwa na vinyago vya kutambikia, huvinyang'anyi nyumbani mwao mwa kuombea? Je? Wewe, unayejivunia kwamba: Ninayo Maonyo, humbezi Mungu kwa kuyakosea Maonyo yake? Kwani Jina lake Mungu hutukanwa kwa wamizimu kwa ajili yenu ninyi, kama ilivyoandikwa. Kwani kutahiri kunafaa, kama unayashika Maonyo. Lakini ukiyakosea Maonyo, kutahiriwa kwako ni kwa bure, utakuwa tena kama mtu asiyetahiriwa. Basi, asiyetahiriwa akiyafuata maongozi ya Maonyo hatawaziwa kuwa kama mwenye kutahiriwa, ijapo hakutahiriwa? Kwa hiyo mtu asiyetahiriwa aliye vivyo hivyo, alivyozaliwa, akiyatimiza Maonyo atakuumbua wewe uliye mwenye Maandiko na mwenye tohara, ukiwa unayakosea Maonyo Kwani Myuda si yeye anayejulikana kwa nje, ya kuwa ni Myuda, nako kutahiriwa siko kule kunakojulikana nje mwilini. Lakini aliye Myuda huko ndani kusikoonwa na watu, yeye ni Myuda. Nako kutahiriwa, kama ilivyoandikwa, siko; kwenye kweli ndiko kutahiriwa kwa moyo kunakowezekana kwa nguvu ya Roho; nako kutasifiwa, lakini siko kwa watu, ila kwa Mungu Ikiwa hivyo, Wayuda wanapitaje wengine? Au kutahiriwa kunafaaje? Hufaa sana hapo na hapo. Kwanza waliagiziwa maneno yake Mungu. Au mwawazaje? Wengine wao wakikataa kuyategemea, huo ukatavu wao utautangua welekevu wake Mungu? La, sivyo! Sharti Mungu ajulikane kuwa mwenye kweli, lakini kila mtu sharti ajulikane kuwa mwenye uwongo, kama ilivyoandikwa: Sharti wongofu wako utokezwe na maneno yako, upate kushinda utakapobishiwa. Lakini upotovu wetu ukiutokeza wongofu wake Mungu, tutasemaje? Je? Mungu naye siye mpotovu akitutolea makali? (Nasema kimtu.) La, sivyo! Mungu angaliwezaje kuuhukumu ulimwengu? Lakini kweli ya Mungu ikiongezwa utukufu na uwongo wangu, mimi tena ninahukumiwaje kama mkosaji? Hivyo sivyo, tunavyosingiziwa, wengine wakitusema sisi, kwamba tumesema: Na tuyafanye yaliyo maovu, yaliyo mema yapate kutokea? Hao hukumu yao inapasa kabisa. Sasa Je? Tumewapita? Hapana, hata kidogo tu. Kwani hapo mbele tumewasuta wote, Wayuda na Wagriki, kwamba: Wote ni wakosaji, kama ilivyoandikwa: Hakuna aliye mwongofu hata mmoja. Hakuna aliye mwenye akili, hakuna anayemtafuta Mungu. Wote pamoja wamepotelewa na njia, wote ni waovu. Hakuna anayefanya mema, hakuna hata mmoja. Makoo yao huwa makaburi yaliyo wazi, ndimi zao huzitumia uwongo tu, sumu ya pili imo midomoni mwao. Vinywa vyao hujaa matusi na uchungu, miguu yao hupiga mbio kuja kumwaga damu. Maangamizo na mavunjiko huzijulisha njia zao, lakini njia ya utengemenao hawaijui. Kumwogopa Mungu hakupo machoni pao. Lakini sisi twajua: Yote, Maonyo yanayosema, huwaambia wenye kuyashika Maonyo, kila kinywa kifumbwe, nao ulimwengu wote uwe umepaswa na hukumu ya Mungu. Kwa hiyo hapo, alipo, hapana mwenye mweli wa kimtu atakayepata wongofu kwa kwamba: Ameyafanya Maonyo, kwa sababu Maonyo huleta utambuzi tu wa makosa. *Lakini sasa wongofu wa Kimungu umefunuliwa pasipo Maonyo; nao unashuhudiwa na Maonyo pamoja na Wafumbuaji kwamba: Wongofu wa Kimungu ndio huu: mwanzo ni kumtegemea Yesu Kristo, nao mwisho: wote wanaomtegemea huupata. Kwani hawapitani, kwa sababu wote wamekosa, wakalipoteza fungu lao la utukufu wa Mungu. Kwa hiyo wanapata wongofu bure tu, kwani ni gawio, Yesu Kristo alilowapatia hapo, alipoyalipa makombozi yao. Ndiye, Mungu aliyemtoa, kusudi wenye kumtegemea wajipatie Kiti cha Upozi katika damu yake; hapo ndipo, alipoonyesha, wongofu wake ulivyo, akiwaondolea makosa ya kale, ambayo Mungu alikuwa akiyavumilia. Hivi ndivyo, alivyouonyesha siku hizi za sasa wongofu wake kuwa hivyo: Mwenyewe ni mwongofu, tena mwenye kumtegemea Yesu humpa wongofu. Basi, majivuno yako wapi? Yamefungiwa! Kwa nguvu ya maonyo gani? Ni yale yanayotaka matendo? Hapana, ni Maonyo yanayotaka kutegemewa tu. Kwani tunalishika hili la kwamba: Mtu hupata wongofu kwa kumtegemea Mungu tu, ijapo asiyatimize Maonyo.* Au je? Mungu ni Mungu wao Wayuda tu? Siye Mungu wa wamizimu nao? Kweli, ni Mungu wa wamizimu nao, kwani Mungu ni mmoja tu; waliotahiriwa huwapatia wongofu, wakiwa wanamtegemea; vilevile wasiotahiriwa huwapatia wongofu, wakiwa wanamtegemea. Je? Ikiwa hivyo, tutayatangua Maonyo kwa kule kumtegemea? Sivyo, tutayasimamisha. Basi, tusemeje? Aburahamu, baba yetu wa kale, kimtu ameonaje? Kwani Aburuhamu, kama alipata wongufu kwa ajili ya matendo yake, kweli analo la kujivunia, lakini mbele ya Mungu haliko. Kwani Maandiko yanasemaje? Aburahamu alimtegemea Mungu, kwa hiyo aliwaziwa kuwa mwenye wongofu. Lakini mtu wa kazi haupati mshahara wake kama kipaji, anachogawiwa, ila kama malipo yanayompasa. Lakini asiye mtu wa kazi akimtegemea anayewapatia wongofu nao wasiomcha Mungu, basi, huyo anapata wongofu kwa kumtegemea Mungu. Ndivyo, anavyosema hata Dawidi kwa kumshangilia mtu, Mungu amwaziaye kuwa mwenye wongofu, ijapo asiyatimize Maonyo. Akasema: Wenye shangwe ndio walioondolewa mapotovu nao waliofunikwa makosa. Mwenye shangwe ni mtu, Bwana asiyemhesabia makosa. Basi, wenye kushangiliwa hivyo ndio waliotahiriwa au wasiotahiriwa nao? Kwani twasema: Aburahamu aliwaziwa kuwa mwenye wongofu kwa kumtegemea Mungu. Ilikuwa lini, alipowaziwa hivyo? Alipokuwa ametahiriwa au alipokuwa hajatahiriwa bado? Sipo hapo, alipokwisha tahiriwa, ila hapo alipokuwa hajatahiriwa bado. Kisha akatahiriwa, apate kielekezo, kiwe kama muhuri ya wongofu uliotoka kwa kumtegemea Mungu, alipokuwa hajatahiriwa bado. Hivyo yeye ni baba yao wote watakaomtegmea Mungu wakiwa hawakutahiriwa; maana nao sharti wawaziwe kuwa wenye wongofu. Vilevile ni baba yao waliotahiriwa; lakini waliotahiriwa nje tu sio; ni wale tu waliotahiriwa, kisha wakakaza kuzifuata nyayo za kumtegemea Mungu, baba yetu Aburahamu alikokuwa nako alipokuwa hajatahiriwa bado. Kwani Maonyo siyo yaliyompatia Aburahamu au wao wa uzao wake kiagio cha kwamba; Urithi wako ni ulimwengu wote; hicho amekipata kwa wongofu uliotoka kwa kumtegemea Mungu. Kama wenye kuyafuata Maonyo wangekuwa nao warithi, kumtegemea Mungu kungekuwa kwa bure, tena kile kiagio nacho kingekuwa kimekwisha kutanguliwa. Kwani Maonyo huleta makali tu; lakini pasipo Maonyo hata kuyakosea hakuna. Kwa hiyo wenye kumtegemea Mungu ndio watakaogawiwa; tena hivyo kile kiagio kinawatimilia wao wote walio uzao wake, sio wenye kuyafuata Maonyo tu, ila nao wenye kuifuata njia yake Aburahamu ya kumtegemea Mungu; hivyo ndivyo, anavyokuwa baba yetu sisi sote, kama ilivyoandikwa: Nimekuweka, uwe baba yao mataifa mengi. Ni kwa sababu alimtegemea Mungu anayewarudisha wafu uzimani, anayeviita visivyokuwapo, vikapata kuwapo. Napo hapo palipokuwa pasipo kingojeo cho chote, alifuliza kukitegemea kingojeo cha kwamba: Atakuwa baba ya mataifa mengi, kama ilivyosemwa: Hivyo ndivyo, wao wa uzao wako watakavyokuwa. Tena kumtegemea Mungu hakukumpungukia napo hapo, alipouona mwili wake, ya kuwa umekufa; maana alikuwa wa miaka kama mia; wala hapo, alipomwona mama yetu Sara, ya kuwa mwili wake umekufa vilevile. Hata kile kiagio cha Mungu hakupotelewa nacho, kwani kukitegemea hakukumshinda, ila akakaza kukitegemea kwa nguvu, akamtukuza Mungu. Maana aliyashika moyoni, aliyoyatambua ya kuwa: Yeye ana nguvu ya kuyatimiza, aliyoyaagia. Hivyo ndivyo, alivyowaziwa kuwa mwenye wongofu. Lakini hilo halikuandikwa kwa ajili yake tu, ya kuwa ndivyo, alivyowaziwa, ila hata kwa ajili yetu, tutakaowaziwa vivyo hivyo tukimtegemea yeye aliyemfufua Bwana wetu Yesu katika wafu, aliyetolewa kwa ajili ya maanguko yetu, akafufuliwa kwa ajili ya wongufu wetu. *Kwa hivyo, tulivyopewa wongofu kwa kumtegemea Mungu, tumekwisha kupata utengemano kwake Mungu; naye aliyetupatia ni Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa kumtegemea yeye tumefunguliwa njia ya kulifikia gawio hili, tunalolikalia, tukajivunia kingojeo cha utukufu, Mungu atakaotupa. Lakini si hiki tu, ila twajivunia hata maumivu, kwani twajua ya kuwa: Maumivu huleta uvumilivu; nao uvumilivu huleta welekevu; nao welekevu huleta kingojeo; nacho kingojeo hakitudanganyi, kwani upendo wa Mungu umemiminiwa mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu, tuliyepewa sisi. Kweli sisi tulikuwa tukingali wanyonge, lakini papo hapo, palipotimia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi tusiomcha Mungu. Kwa watu mtu hushindwa kuuawa kwa ajili ya mwongofu; labda atapatikana anayejipa moyo wa kufa kwa ajili yake yeye aliye mwema. Lakini jinsi ulivyo upendo wake Mungu wa kutupenda sisi, vimetokea waziwazi hapo, Kristo alipokufa kwa ajili yetu sisi, tukingali wakosaji. Sasa je? Kwa hivyo, damu yake ilivyotupatia wongofu, hatutazidi kuokolewa naye, makali yasitupate kamwe? Hapo, tulipokuwa tunamchukia Mungu, Mwanawe akawa kole, akatukomboa kwa kufa kwake; sasa je? Kwa hivyo, tulivyokwisha kukombolewa, hatutaokolewa po pote kwa nguvu ya uzima wake? Lakini si hili tu, tunalojivunia, ila twajivunia hata Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwa sababu hata sasa tunapata makombozi kwake.* Kwani ni hivi: Makosa yaliingizwa ulimwenguni na mtu mmoja, kisha kufa kuliingizwa na makosa, nako kufa kumewafikia watu wote, kwa maana walikosa wote. Hapo, Maonyo yalipotokea, makosa yalikuwamo ulimwenguni; lakini makosa hayahesabiwi pasipo Maonyo. Lakini tangu Adamu mpaka Mose kifo kilishika ufalme hata kwao wale wasiokosa, kama Adamu alivyokosa kwa kubeza agizo. Naye ni mfano wake yeye aliyetazamiwa, atokee siku za halafu. Lakini kuanguka kulivyo, sivyo nako kugawiwa mema kulivyo. Maana wengi walikufa kwa ajili ya anguko la yule mmoja; lakini magawio ya Mungu tumegawiwa bure, ni kipaji cha yule mtu mmoja Yesu Kristo, kikawafurikia wengi. Tena nguvu ya kipaji hiki na nguvu ya yule mkosaji mmoja hazifanani: maana kuhukumiwa kwa mmoja kuliwaletea wote maangamizo; lakini hilo gawio linaondoa maanguko mengi, likigawia wongofu. Kwani anguko la mmoja ndilo lililokipatia kifo ufalme, kikaushika kwa ajili yake yeye mmoja; lakini wao waliogawiwa mafuriko ya hicho kipaji kikubwa cha kupewa wongofu bure tu watashika ufalme uzimani kuupita ule kwa ajili yake yeye mmoja Yesu Kristo. Basi, ni hivi: Anguko la mmoja liliwapatia watu wote maangamizo, vivyo hivyo wongofu wa mmoja uliwapatia watu wote wongofu unaowapa uzima. Kwani kama wengi walivyotokezwa kuwa wakosaji kwa ajili ya ukatavu wa mtu mmoja, vivyo hivyo wengi wanatokezwa kuwa wenye wongofu kwa ajili ya usikivu wake yule mmoja. Lakini Maonyo yaliingia hapo kati, maanguko yaongezeke. Lakini makosa yalipokuwa mengi, ndipo, magawio yalipofurika. Kama makosa yalivyoshika ufalme wa kuua watu, vivyo hivyo nayo magawio sharti yashike ufalme wa kuwapa watu uzima wa kale na kale kwa nguvu ya wongofu, aliotupatia Bwana wetu Yesu Kristo. Sasa tusemeje? Tufulize kukosa, magawio nayo yafurike? La, sivyo! Sisi tulioyafia makosa tutawezaje kuishi nayo tena? *Au hamjui, ya kuwa sote tuliobatiziwa, tuwe wake Kristo Yesu, tulibatiziwa, tufe naye? Hivyo tulizikwa pamoja naye tulipobatiziwa, tufe naye, ni kwamba: Kama Kristo alivyofufuliwa katika wafu kwa nguvu ya utukufu wa Baba, vivyo nasi sharti tupate upya wa maisha, tuendelee nao. Kwani tulivyounganika naye tulipokufa, kama alivyokufa, vivyo tutafufuka nasi, kama alivyofufuka yeye. Kwani tunalitambua neno hili: mtu wetu wa kale amewambwa msalabani pamoja naye, miili yetu yeye kukosa ipate kukomeshwa, sisi tusiyatumikie tena makosa kama watumwa. Kwani aliyekufa amekwisha kupata wongofu kwa kuondolewa kwenye makosa. Nasi kama tumekufa pamoja na Kristo, tunalitegemea la kwamba: Tutaishi pamoja naye. Kwani twajua, ya kuwa Kristo hafi tena kwa hivyo, alivyofufuliwa katika wafu, kifo hakina ufalme tena wa kumshika. Kwani hivyo, alivyokufa, aliyafia makosa na kuyashinda papo hapo; lakini hivyo, anavyoishi, anaishi, amtumikie Mungu. Nanyi jiwazieni hivyo: makosa mmekwisha kuyafia, lakini sasa mnaishi, mmtumikie Mungu katika Kristo Yesu!* Kwa hiyo ukosaji usishike ufalme katika miili yenu yenye kufa, mzitii tamaa zao! Wala msivitoe viungo vyenu, viwe mata ya upotovu ya kuyatumikia makosa! Ila mjitoe wenyewe kumtumikia Mungu kwa hivyo, mnavyoishi, tena mlikuwa mmekwisha kufa! Navyo viungo vyenu mvitoe, viwe mata ya wongofu ya kumtumikia Mungu! Kwani ukosaji hautashika ufalme, uwatawale, maana nguvu yenu siyo ya Maonyo, ila ya upole. Basi, inakuwaje? Tukose vivyo hivyo, kwa sababu nguvu yetu siyo ya Maonyo, ila ya upole? La sivyo! Hamjui, vilivyo? Ni hivi: mnapojitoa wenyewe kumtumikia mtu kitumwa na kumtii, basi, mmekwisha kuwa watumwa wake yeye, mnayemtii. Ikiwa ni wa ukosaji, mnakwenda kufa; ikiwa ni wa wito, mnakwenda kupata wongofu. Lakini Mungu atolewe shukrani, kwa sababu ninyi mliokuwa watumwa wa ukosaji mmegeuzwa mioyo, mkaja kuyatii mafundisho, kama mlivyoyapata! Napo hapo, mlipokombolewa katika utumwa wa ukosaji, mmegeuka kuwa watumwa wa wongofu. *Nasema kimtu kwa ajili ya unyonge wa miili yenu: Kama mlivyovitoa viungo vyenu kuutumikia kitumwa uchafu na upotovu, mkajifikisha penye kupotolewa, vivyo hivyo vitoeni sasa viungo vyenu kuutumikia kitumwa wongofu, mjifikishe penye kutakaswa! Kwani mlipokuwa watumwa wa ukosaji, siku zile mlikuwa hamna wongofu hata kidogo. Basi, siku zile mlikuwa na mapato gani? Sasa hivi mnayaonea soni, kwani mwisho wao ni kufa. Lakini sasa kwa kuwa mmekwisha kukombolewa katika utumwa wa ukosaji, mkawa watumwa wake Mungu, mnayo mapato yenu kwa kujifikisha penye kutakaswa, tena mwisho mtapata uzima wa kale na kale. Kwani mshahara wa ukosaji ni kufa; lakini gawio, Mungu analotupa katika Bwana wetu Kristo Yesu, ni uzuma wa kale na kale. Na niseme nanyi, kwa kuwa mnayatambua Maonyo: Hamjui, ndugu: Maonyo humshika mtu siku zote za maisha yake? Kwani mwanamke aliye na mume siku za kuishi kwake mumewe ana mwiko kwa ajili ya Maonyo; lakini nguvu ya hayo Maonyo hukoma, mumewe anapokufa, hana mwiko tena wa mwanamume mwingine. Siku za kuishi kwake mumewe, yeye akiwa wa mume mwingine, huitwa mzinzi. Lakini mumewe anapokufa, amefunguliwa na Maonyo, asiwe tena mzinzi akiwa wa mume mwingine. Ndugu zangu, hapo Kristo alipokufa, mliuawa nanyi, mkayafia Maonyo; kwa hiyo mmefunguliwa nanyi kuwa wa mwingine, maana ni wa yule aliyefufuliwa katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda. Kwani hapo, mwenendo wetu ulipokuwa wa kimtu, tamaa mbaya zikatuumiza sana, nazo nguvu zao zikaongezeka tu katika viungo vyetu kwa kukatazwa na Maonyo, tukakizalia kifo matunda. Lakini sasa tumefunguliwa, hiyo nguvu ya Maonyo isitushike, tukamfia yule aliyetupinga; hivyo ndivyo, utumikizi wetu ulivyopata kuwa mpya wa kiroho, wa kale uliokuwa wa utumwa wa maandiko ukome. *Sasa tusemeje? Maonyo hukosesha? La, sivyo! Lakini kosa singelitambua pasipo Maonyo. Kwani hata tamaa singeijua, kama Maonyo yasingesema: Usitamani! Lakini ukosaji ulianzia hapohapo penye agizo hilo, ukakuza moyoni tamaa yo yote, ukaitia nguvu; kwani pasipo Maonyo ukosaji ni mfu. Nami kale nilikuwa ninaishi pasipo Maonyo; lakini agizo lilipokuja, ukosaji ukafufuka, nami nikafa; hivyo agizo lililotokea, linipe uzima, likaonekana, ya kuwa ni lilo hilo lililoniua. Kwani ukosaji ulianzia hapohapo penye agizo hilo, ukanidanganya, ukaniua kwa hilo agizo. Kwa hiyo Maonyo ni matakatifu, nalo agizo ni takatifu lenye wongofu na wema. Basi, inakuwaje? Lililo jema ndio lililoniua mimi? La, sivyo! Ila ukosaji ndio ulioniua; lakini kusudi uonekane kuwa ukosaji, ukaniua kwa lile lililo jema; kwa hivyo, ukosaji ulivyolitumia lile agizo, ukatokea wazi kuwa ukosaji wenyewe usiozuilika kabisa. Kwani Maonyo tunayajua, ya kuwa ni ya Kiroho; lakini mimi ni wa kimtu, nikauzwa kuwa mtumwa wa ukosaji. Kwani siyatambui, ninayoyatenda: kwani ninachokitaka sikifanyi, ila ninachokichukia, ndicho, ninachokifanya. Nami nisichokitaka, ninapokifanya hichohicho, basi, ninayaitikia Maonyo kuwa mazuri.* Sasa si mimi ninayekifanyiza hicho, ila ndio ukosaji unaonikalia moyoni. Kwani najua: Humu ndani yangu, maana mwilini mwangu, hamna chema cho chote; kama ni kutaka, ninako, lakini kama ni kukifanya kilicho kizuri, sinako. Kwani kilicho chema, ninachokitaka, sikifanyi; ila kilicho kiovu, nisichokitaka, ndicho, ninachokifanyiza. Lakini mimi nisichokitaka, ninapokifanya hichohicho, basi, si mimi tena ninayekifanya, ila ndio ukosaji unaonikalia moyoni. Hivyo mimi ninayetaka kukifanya kilicho kizuri, ninaona nguvu ngeni kwangu inayonishurutisha kukifanya kilicho kiovu. Kwani ninayaitikia Maonyo yake Mungu na kuyashangilia huku ndani moyoni. Lakini naona, yamo maonyo mengine viungoni mwangu yanayoyagombeza Maonyo yaliyomo rohoni mwangu, yakaniteka kuwa mtumwa wa maonyo yanayonikosesha, ndiyo yale yaliyomo viungoni mwangu. Yamenipata mimi mtu mkiwa! Yuko nani atakayenikomboa utumwani mwa mwili huu wa kufa? Mungu atolewe shukrani kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo! Basi, kwa akili zangu mimi mwenyewe nayatumikia kitumwa Maonyo yake Mungu, lakini mwilini ni mtumwa wa maonyo ya ukosaji. *Sasa hakuna tena kinachowapatiliza walio katika Kristo Yesu, wasioendelea kimtu, ila Kiroho. Kwani Maonyo ya Roho inayotupatia uzima katika Kristo Yesu yamenikomboa utumwani mwa maonyo ya ukosaji yaliyoniua. Kwani vile, ambavyo Maonyo hayakuweza kuvimaliza kwa ajili ya unyonge wa miili ya kimtu, Mungu alivifanya alipomtuma Mwana wake mwenyewe; akaja mwenye mwili wa makosa, akakamatwa kuwa kole ya makosa; hivyo ndivyo, alivyoyapatiliza makosa katika mwili ulio wa kimtu, wongofu unaotakwa na yale Maonyo utimilizike mioyoni mwetu sisi, tusioendelea kimtu, ila Kiroho. Kwani walio wa kimtu huyawaza mambo ya kimtu, lakini walio wa Kiroho huyawaza mambo ya Kiroho. Kwani mawazo ya kimtu huleta kufa; lakini mawazo ya Kiroho huleta uzima na utengemano. Kwa sababu hiyo mawazo ya kimtu humchukia Mungu; kwani hayataki kuyatii Maonyo ya Mungu, wala hayawezi kuyatii; kwa hiyo walio wa kimtu hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ninyi ham wa kimtu, ila wa Kiroho, kama Roho ya Mungu inawakalia mioyoni; lakini asiye na Roho ya Kristo huyo si wake. Lakini Kristo akiwakalia mioyoni, kweli miili itakufa kwa ajili ya makosa, lakini roho zitaishi kwa ajili ya wongofu. Lakini Roho yake yule aliyemfufua Yesu katika wafu ikiwakalia mioyoni, yuyu huyu aliyemfufua Yesu Kristo katika wafu atairudisha uzimani hata miili yenu, itakapokwisha kufa; atayafanya kwa nguvu ya Roho yake inayowakalia mioyoni. *Kwa hiyo, ndugu, hatumo tena katika udeni wa miili yetu ya kimtu, tuendelee kimtu; kwani mnapoendelea kimtu mtakufa. Lakini mnapoyaua matendo ya miili yenu ya kimtu kwa nguvu ya Roho mtapata kuishi. Kwani wote wanaoongozwa na Roho ya Mungu hao ndio wana wa Mungu. Kwani hamkupewa tena roho ya kitumwa, mshikwe na woga, ila mmepewa Roho ya kimwana, ndiyo inayotufundisha kuomba: Ee, Baba yetu! Hiyo Roho yake yenyewe huzishuhudia roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wake Mungu. Lakini tukiwa watoto, basi, tunakuwa hata warithi, maana warithi wake Mungu watakaopata urithi pamoja na Kristo; tukiwa tunateswa pamoja naye tutapata hata kutukuzwa pamoja naye. *Kwani naona, ya kuwa mateso ya siku hizi za sasa si kitu, tukiyafananisha na ule utukufu, tutakaofunuliwa sisi. Kwani viumbe vyote vinavumilia na kuyachungulia matokeo ya wana wa Mungu. Kwani viumbe vimewekwa, vioze, si kwa mapenzi yao wenyewe, ila kwa ajili yake aliyeviweka hivyo; navyo viko na kingojeo chao. Kwani viumbe navyo vitakombolewa katika utumwa wa kuoza, viingie navyo uungwana uliomo katika utukufu wa watoto wake Mungu. Kwani twajua, ya kuwa viumbe vyote vipo pamoja nasi vikipiga kite kwa kuona uchungu mpaka sasa hivi. Tena sivyo hivyo tu, ila na sisi wenyewe tuliokwisha pata malimbuko ya Roho twapiga kite ndani mioyoni tukichungulia kuwa wana, kwani ndipo, miili yetu nayo itakapokombolewa. *Kwani kingojeo, ambacho tuliokolewa, tuwe nacho, hicho ndicho; lakini kingojeo kinachoonekana machoni sicho kingojeo. kwani hilo, mtu analoliona, analingojeaje? Lakini tusiloliona, tukilingojea, tunalichungulia kwa kuvumilia. Hivyo hata Roho hutusaidia sisi tulio wanyonge. Kwani tusipojua maombo yanayopasa, hapo Roho mwenyewe hutuombea, tukipiga kitekite tu kisichosemekana. Lakini yeye nayeipeleleza mioyo ameyajua mawazo ya Roho, kwani huwasemea watakatifu Kimungu.* Tunajua, ya kuwa: Kwao wanaompenda Mungu mambo yote husaidiana kuwapatia mema; ndio hao, aliowaita kwa yale, aliyowawekea kale. Kwani aliowatambua kale, ndio, aliowachagua kale, wafanane na Mwana wake wakiwa sura moja naye, yeye apate kuwa Kibwana katika wanduguze wengi. Nao aliowachagua kale, hao ndio, aliowaita; nao aliowaita, hao ndio aliowapa wongofu; nao aliowapa wongofu, hao ndio, aliowatukuza. Hayo yote tuyasemeje? Mungu akiwa upande wetu, yuko nani atakayetushinda? Hakumwonea Mwana wake mwenyewe uchungu, ila alimtoa kwa ajili yetu sisi sote; kwa hiyo asitupatie sisi magawio yote kwake yeye?* *Yuko nani atakayewasuta waliochaguliwa na Mungu? Mungu yuko anayewashuhudia kuwa waongofu. Yuko nani atakayewahukumu? Kristo Yesu yuko aliyekufa kwa ajili yao, na kupita hapo amefufuka, yuko kuumeni kwa Mungu na kutusemea sisi. Yuko nani atakayetutenga na upendo wake Kristo? Maumivu au masongano au mafukuzo au njaa au uchi au maponzo au panga? Ndivyo vilivyoandikwa kwamba: Kumbe ni kwa ajili yako wewe, tukiuawa kila siku tukihesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa tu! Lakini katika mambo hayo yote tunazidi kushinda kabisa kwa nguvu yake yeye aliyetupenda sisi. Kwani hili nimelitambua kuwa kweli kabisa: Kukiwa kufa au kuishi, wakiwa malaika au wenye nguvu, yakiwa ya leo au ya kale, zikiwa nguvu za mbinguni juu au za kuzimuni chini, vikiwa viumbe vyo vyote vingine, hakuna kitakachoweza kututenga sisi na upendo wake Mungu uliotutokea katika Kristo Yesu, Bwana wetu.* Kristo anajua: nasema kweli, sisemi uwongo; hata moyo wangu unaoyajua hunishuhudia katika Roho takatifu, ya kuwa masikitiko yangu ni makubwa, nao uchungu haukomi moyoni mwangu. Kwa hiyo naliomba mara kwa mara, mimi mwenyewe niapizwe, niondolewe kwake Kristo, kama hivyo vingeweza kuwaponya ndugu zangu, ambao tulizaliwa nao kimtu. Kweli ndio Waisiraeli, tena ni wana, hata utukufu wanao, walipewa maagano na maonyo na tambiko lililo la kweli na viagio. Wanao hata baba, namo miongoni mwao ndimo, Kristo alimozaliwa kimtu; huyu ni mkubwa kuwapita wote, ni Mungu, atukuzwe kale na kale! Amin. Lakini sisemi hivyo, kwamba Neno lake Mungu limetenguka. Kwani walio kizazi chake Isiraeli sio wote Waisiraeli. Wala walio wa uzao wake Aburahamu sio wote hata watoto. Ila imeandikwa: Watakaoitwa uzao wako ni wa Isaka tu. Ni kwamba: Walio watoto wa kimtu hao sio watoto wake Mungu; ila walio watoto wa kiagio huwaziwa kuwa uzao. Kwani neno la kiagio ni hilo la kwamba: Nitakapokuja siku zizi hizi za mwaka ujao, ndipo, Sara atakapokuwa mwenye mtoto wa kiume. Lakini hivyo haikuwa hapo tu, ilikuwa napo hapo, Rebeka alipopata mimba kwake yule mmoja aliye baba yetu Isaka. Kwani hapo, watoto walipokuwa hawajazaliwa, wala hawajafanya mema au maovu, hapo ndipo, Mungu alipowachagulia kwa hivyo, alivyowawekea kale, viwepo. Vikawapo, si kwa ajili ya matindo yao, ila kwa wito wake yeye. Kwa hivyo Rebeka aliambiwa: Mkubwa atamtumikia nduguye. Ndivyo, ilivyoandikwa: Nilimpenda Yakobo, lakini Esau nilimchukia. Basi, tusemeje? Kwa Mungu uko upotovu? La, sivyo! Kwani anamwambia Mose: Nitakayemhurumia, nitamhurumia kweli; nitakayemwonea uchungu, nitamwonea uchungu wa kweli. Kwa hiyo kutaka kwa mtu siko, wala mbio zake sizo, ila Mungu mwenye huruma ndiye yeye tu. Kwani Maandiko yanamsema Farao: Kwa sababu hiihii nimekuweka, niionyeshe nguvu yangu kwako wewe, Jina langu lipate kutangazwa katika nchi zote. Kwa hiyo humhurumia, anayemtaka; tena humshupaza, anayemtaka. Labda utaniambia: Mbona hutukamia? Kwani yuko nani ayapingaye mapenzi yake? Mwenzangu, u mtu gani ukitaka kubishana na Mungu? Je? Kiko chombo kitakachomwambia muumbaji: Mbona umenifanya hivi? Mfinyanzi haufanyishi udongo, kama anavyotaka? Donge lililo moja upande mmoja haliumbi kuwa chombo kizuri, nao upande mwingine kuwa kibaya? Inakuwaje? Ni kweli, Mungu anataka kuyaonyesha makali yake, tena anataka kuutambulisha uwezo wake, lakini kwa uvumilivu wake mwingi aliwavumilia walio vyombo vitakavyo makali tu, vilivyotengenezwa, viangamie tu. Kisha anataka kuutambulisha hata wingi wa utukufu wake kwao walio vyombo vitakavyo huruma, ndio, aliowapatia utukufu kale; nao ndio, aliowaita kwenye Wayuda nako kwenye wamizimu, nasi tumo. Ndivyo, anavyosema hata kinywani mwa Hosea: Aliitwa: Si ukoo wangu nitamwita: Ukoo wangu, naye asiyependwa nitamwita Mpendwa. Itakuwa hapo, hao wanaoambiwa sasa: Ninyi ham ukoo wangu, waambiwe: M wanawe Mungu aliye Mwenye uzima. Naye Yesaya anawasemea Waisiraeli na kupaza sauti: Wana wa Waisiraeli ijapo wawe wengi kama mchanga wa ufukoni, watakaookoka watakuwa sao tu. Kwani Bwana ndiye atakayevimaliza, atakapolitimiza Neno lake nchini kwa kulikata. Navyo ndivyo, Yesaya alivyosema kale: Bwana Mwenye vikosi kama asingalitusazia uzao, tungalikuwa kama Sodomu, tungalifanana na Gomora. Basi, tusemeje? Ni hivi: Wamizimu wasiofuata wongofu wamepata wongofu; ni wongofu ule unaopatikana kwa kumtegemea Mungu. Lakini Waisiraeli walioyafuata Maonyo yenye wongufu hawakuyafikia hayo Maonyo. Kwa sababu gani? Kwa sababu walikataa kumtegemea Mungu, wakafanya mambo yao tu. Wakajigonga katika lile jiwe la kujigongea, kama ilivyoandikwa: Tazama, naweka humo Sioni jiwe la kujigongea na mwamba wa kujikwalia. Naye alitegemeaye hatatwezeka. *Ndugu, moyo wangu unayapenda sana, ninayomwomba Mungu kwamba: Waisiraeli waokoke. Kwani nawashuhudia, ya kuwa waona wivu kwa ajili yake Mungu, lakini hawamtambui. Kwani wongofu, Mungu anaoutaka, hawaujui, wakajaribu kujiongoza wenyewe, lakini hivyo hawakuutii ule wongofu, Mungu anaoutaka. Kwani timilizo la Maonyo ni Kristo, kila mwenye kumtegemea ajipatie wongofu! Kwani Mose aliandika: Anayeufanya wongofu ulioagizwa na Maonyo mtu huyo atapata uzima kwa njia hiyo. Lakini wongofu unaopatikana kwa kumtegemea Mungu unasema hivyo: Usiseme moyoni mwako: Yuko nani atakayepaa kwenda mbinguni? Huko ndiko kumshusha Kristo. Wala usiseme: Yuko nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? Huko ndiko kumpaza Kristo na kumtoa kwenye wafu. Tena unasema: Neno hilo linakukalia karibu, limo kinywani mwako, namo moyoni mwako. Hilo ndilo neno la kumtegemea Mungu, ni hilihili, tunalolitangaza. Kwani ukiungama kwa kinywa chako kwamba: BWANA NI YESU, ukamtegemea kwa moyo wako kwamba: Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwani ukimtegemea kwa moyo unapata wongofu; ukimwungama kwa kinywa unaokoka. Kwani Maandiko yasema: Kila anayemtegemea hatatwezeka. Kwani hapa hawachaguliwi Wayuda na Wagriki; kwani aliye Bwana wao wote ni yuyu huyu mmoja, ni mwenye magawio yanayowatoshea wote wanaomtambikia. Kwani; Kila atakayelitambikia Jina la Bwana ataokoka. Basi, watamtambikiaje, wasiyemtegemea? Tena watamtegemeaje, ambaye hawajamsikia Neno lake? Tena watasikiaje, pasipokuwapo mwenye kutangaza? Tena watatangazaje, wasipotumwa? Ndivyo ilivyoandikwa: Tazameni, miguu yao wapiga mbiu njema jinsi inavyopendeza!* Lakini walioutii huo Utume mwema sio wote. Kwani Yesaya anasema: Bwana, yuko nani anayeutegemea utume wetu? Basi, kumtegemea Mungu huletwa na matangazo, lakini matangazo hutoka katika Neno la Kristo. Lakini niseme: Hawakusikia? Kusikia wamesikia. Uvumi wao ulitokea katika nchi zote; nayo maneno yao yalifika hata mapeoni kwa ulimwengu. Au niseme: Waisiraeli hawakulitambua? Kwanza Mose anasema: Mimi na niwachokoze ninyi nikiwaletea watu wasio watu, na niwakasirishe ninyi nikiwaletea taifa la watu wasiojua maana. Kisha Yesaya anajipa moyo wa kusema: Nimeonwa nao wasionitafuta, nikawatokea wasioniuliza. Lakini Waisiraeli anawaambia: Mchana kutwa naliikunjua mikono yangu, nipungie ukoo wa watu wasioonyeka, walio wabishi tu. Basi, niseme: Mungu aliwatupa walio ukoo wake? La, sivyo! Kwani hata mimi ni Mwisiraeli, ni wa uzao wake Aburahamu, ni wa shina la Benyamini. Mungu hakuwatupa walio ukoo wake, aliowatambua kale. Au hamyajui, Maandiko yanayoyasema, Elia alipomlalamikia Mungu kwa ajili ya Waisiraeli? Akasema: Bwana, wafumbuaji wako wamewaua, wakapabomoa pote pa kukutambikia, nikasalia mimi peke yangu, tena roho yangu nayo wanaitafuta, waichukue. Lakini jibu la Mungu linamwambia nini? Nimejisazia watu 7000 wasiompigia Baali magoti. Basi, vivyo hata siku hizi za sasa liko sazo lililochaguliwa kupata magawio. Lakini yakiwa magawio, siyo malipo ya matendo. Kama sivyo, magawio hayangekuwa magawio, kwani kama huko ni kulipa matendo, siko kugawia; kama sivyo, matendo yangekuwa ya bure. Basi inakuwaje? Waisiraeli waliyoyatafuta, hawakuyafikia, lakini wachaguliwao tu ndio walioyafikia. Lakini wale wengine walishupazwa mioyoni mwao, kama ilivyoandikwa: Mungu aliwapa roho ya usingizi na macho yasiyoona na masikio yasiyosikia mpaka siku hii ya leo. Naye Dawidi anasema: Sharti meza zao ziwawie matanzi na mitego, wanaswe, walipizwe mabaya yao. Macho yao na yatiwe giza, wasione, migongo yao nayo ipindike siku zao zote! Basi, niseme: Walijikwalia, waanguke tu? La, sivyo! Ila maanguko yao yamewaletea wamizimu wokovu, wenyewe wawaonee wivu, wapate kujikaza. Lakini maanguko yao yakiwa yameuletea ulimwengu mapato mengi, nako kushindwa kwao kukiwa kumewaletea wamizimu mapato mengi, je? Hapo, watakapokuja wote, hayo mapato hayataongezeka sanasana? Nasema nanyi mlio wamizimu. Mimi kwa hivyo, nilivyo mtume wa wamizimu, na niutukuze utumishi wangu! Hivyo labda nitawatia wivu walio ndugu zangu kimtu, nipate kuwaokoa mmojammoja. Kwani hapo walipotupwa waliwapatia wao wa ulimwengu wokovu; basi, hapo watakapopokelewa watawapatia nini, isipokuwa kufufuka na kutoka penye wafu? Tena limbuko likiwa linatakata, limbiko nalo litatakata. Tena shina likiwa limetakata, matawi nayo yatatakata. Lakini kama yako matawi yaliyovunjwa na kuondolewa, kisha wewe uliye mdanzi tu ukatiwa mahali pao, ukagawiwa fungu lako la shina na utomvu wa ule mchungwa, usijivune kwao yale matawi! Lakini ukijivuna ujue: si wewe unaolipa shina nguvu, ila shina linakupa nguvu wewe! Labda utasema: Matawi yalivunjiwa mimi, nipate pa kutiwa. Ni vizuri; yalivunjika mle, kwa ajili hayakushikamana; wewe nawe ukashinda mle kwa nguvu ya kushikamana. Usijikweze, ila uogope! Kwani Mungu kama asivyoyaonea uchungu yale matawi yaliyochipukia mlemle, hata wewe hatakuonea uchungu. Basi, humo utazame utu na ukali wake Mungu! Ukali uko kwao walioanguka, lakini kwako wewe uko utu wake Mungu, ukifuliza kuukalia huo utu. Ikiwa sivyo, hata wewe utakatwa. Nao wale watatiwa tena, wasipofuliza kuukalia ukatavu; maana Mungu yuko na nguvu ya kuwatia mle tena. Tazama: Wewe ulichipuka katika mdanzi, kisha ukakatwa humo, ukatiwa katika mchungwa usio shina lako; basi, wale waliochipukia mlemle, ni vigumu gani kuwatia tena katika mchungwa wao wenyewe? Kwani sitaki, ndugu, mkose kulijua fumbo hili, mkajiwazia wenyewe kuwa wenye akili. Waisiraeli wengine wao wameshupazwa mioyoni, mpaka wingi wa wamizimu utakapokwisha kuingia. Hivyo ndivyo, Waisiraeli wote watakavyookoka, kama ilivyoandikwa: Mle Sioni atatokea mponya; ndiye atakayemgeuza Yakobo, aache mabezo. Nalo hili ni agano, ninalolifanya nao: Nitayaondoa makosa yao. Kwa hivyo, wanavyoukataa Utume mwema, ndio wachukivu kwa ajili yenu; lakini kwa hivyo, walivyochaguliwa, ndio wapendwa kwa ajili ya baba zao. Kwani Mungu hayajutii magawio na wito wake. Kama ninyi: Kale mlimkataa Mungu, lakini sasa mmehurumiwa kwa ajili ya ukatavu wao hao; vivyo hivyo hata hao sasa wameikataa ile huruma iliyowatokea, kwamba nao siku ziwafikie, watakapohurumiwa. Kwani Mungu aliwaunga wote pia, wamkatae, apate kuwahurumia wote. *Tazameni, jinsi ujuzi na utambuzi wake Mungu unavyofurika kuwa mwingi! Kweli maamuzi yake hayachunguziki, njia zake nazo hazinyatiliki! Kwani yuko nani aliyeyatambua mawazo ya Bwana? Au yuko nani aliyekula njama naye? Au yuko nani aliyeanza kumpa kitu, apate kulipwa naye? Kwani yote yalitoka kwake yeye, yakafanywa naye yeye, tena yatarudi kwake yeye. Yeye ndiye atakayetukuzwa kale na kale. Amin.* *Nawaonya, ndugu, kwa hivyo, Mungu alivyowaonea uchungu, mtoe miili yenu, iwe vipaji vitakatifu vya tambiko vyenye uzima vya kumpendeza Mungu; huko ndiko kumtumikia Mungu kunakoelekea. Msijifananishe nao walio wa siku hizi tu, ila mgeuke, mpewe mawazo mapya, mpate kuyapambanua, Mungu ayatakayo kwamba: Ni mema ya kumpendeza hapo, yatakapotimilika. Kwa kipaji, nilichogawiwa, namwambia kila mmoja wa kwenu, asiwaze makuu yanayopapita hapo panapopasa kuwaza. Ila awaze, jinsi atakavyopata kuerevuka, kila mtu, kama Mungu alivyomgawia kumtegemea. Kwani ni vivyo hivy: tunavyo viungo vingi katika mwili mmoja, lakini viungo vyote havina kazi moja. Vivyo sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa maana tu wa Kristo, tena kila mmoja na mwenzake tu viungo tu. Tena vipaji, tulivyopewa ni vingi, kila mtu anacho chake, kama alivyogawiwa.* *Mwenye ufumbuaji sharti aupatanishe na kumtegemea Mungu. Mwenye utumishi sharti atumike kweli! Mfunzi na aushike ufundisho wake! Mwenye kuonya sharti aonyeke! Mwenye kugawia sharti anyenyekee! Aliye mkuu sharti ajihimize! Mwenye kutunza wengine sharti avifurahie! Mapendano yasiwe ya uwongo! Yachukieni yaliyo mabaya mkigandamiana nayo yaliyo mema! Mpendane kindugu kwa mioyo, tena mwongozane na kuheshimiana ninyi kwa ninyi! Msilegee, panapotakwa wenye kujikaza! Roho zenu ziwe zenye moto mnapomtumikia Bwana! Furahini, ya kwamba mnacho kingojeo! Yavumilieni maumivu! Fulizeni kuomba! Changeni bia, mwapatie watakatifu, wanavyovikosa! Wageni wapokeeni pasipo kunung'unika! Changeni bia, mwapatie watakatifu, wanavyovikosa! Wageni wapokeeni pasipo kunung'unika! Furahini pamoja nao wafurahio! Lieni pamoja nao waliao! Mioyo yenu nyote sharti iwe mmoja! Msiyatunukie yaliyo makuu, ila yaliyo manyonge, mfuatane nayo! Msijiwazie wenyewe kuwa wenye akili!* *Msimlipe mtu maovu kwa maovu! Yawazeni yaliyo mazuri mbele ya watu wote! Kwa hivyo, mlivyo, mwe wenye kupatana na watu wote, ikiwezekana! Wapendwa, msijilipize wenyewe, ila jitengeni, makali (ya Mungu) yapate kutokea! Kwani imeandikwa: Bwana anasema: Lipizi ni langu mimi, ni mimi nitakayelipisha. Lakini mchukivu wako akiwa ana njaa, mpe chakula! Akiwa ana kiu, mpe cha kunywa! Kwani ukivifanya hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe nayo yaliyo maovu, ila maovu uyashinde kwa mema!* *Kila mtu na autii ukuu! Maana uko na nguvu kumpita yeye. Kwani hakuna ukuu usiotoka kwa Mungu; nao wote ulioko umewekwa na Mungu. Kwa hiyo mwenye kuubisha ukuu hulibisha tengenezo lake Mungu. Lakini wabishi watajipatia hukumu. Kwani wenye nguvu hawaogopeshi, ukifanya mema, ila ukifanya maovu. Nawe usipotaka kuuogopa ukuu, fanya yaliyo mema! Hivyo utapata kusifiwa nao. Kwani ukuu humtumikia Mungu, ukupatie mema. Lakini unapofanya maovu ogopa! maana haushiki upanga bure tu. Kwani humtumikia Mungu, humlipiza kwa ukali kila afanyaye kiovu. Kwa hiyo inatupasa kutii, si kwa ajili ya ukali tu, ila hata kwa ajili ya mioyo, itung'ae. Kwa hiyo mnatoa hata kodi, kwani wao ni watumishi wa Mungu wanaoifuliza kazi hiihii tu. Basi, walipeni wote yawapasayo: Mtoza kodi mpeni kodi yake! Mwenye kuchanga mpeni chango lake! Mwenye kuogopesha mwogopeni! Mwenye kuheshimiwa mheshimuni! Msiwe wadeni wa mtu ye yote, isipokuwa wa kupendana! Kwani anayempenda mwenziwe ameyatimiza Maonyo. Kwani kule kwamba: Usizini! Usiue! Usiibe! Usishuhudie uwongo! Usitamani! na kama liko agizo jingine, yanaunganika yote katika neno hili: Umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwenyewe! Ukimpenda mwenzio huwezi kumfanyia kiovu. Kwa hiyo kupendana ndiko kuyatimiza Maonyo.* *Fanyeni hivyo mkizijua siku hizi, kwamba saa imekwisha fika ya kuamka katika usingizi! Maana wokovu wetu sasa uko karibu kuliko siku zile, tulipoanza kumtegemea Bwana. Usiku umefikia kucha, mchana upambazuke: kwa hiyo tuziache kazi za giza, tujivike mata ya mwanga! Tushike mwenendo upasao mchana! Tusiwe walafi na walevi, wala wagoni na waasherati, wala wagomvi na wenye wivu! Ila jivikeni Bwana Yesu Kristo! Itunzeni miili yenu na kuiangalia, isishindwe na tamaa!* Aliye mnyonge wa kumtegemea Bwana mpokeeni pasipo kubishana naye mawazo ya moyo! Mwingine anayategemea ya kwamba: Vyote vinaliwa; mwingine aliye mnyonge hula maboga tu. Mwenye kula asimbeze asiyekula! Wala asiyekula asimwumbue mwenye kula! Kwani Mungu amempokea. Wewe u nani ukimwumbua mtumishi wa mwingine? Akiwa amesimama au akiwa ameanguka, yote humfanyizia Bwana wake mwenyewe. Lakini atainuliwa, kwani Bwana anaweza kumwinua. Mwingine huchagulia siku za kuzitakasa, mwingine huzitakasa siku zote. Kila mtu sharti afulize kuyafuata, aliyoyatambua yeye kuwa ya kweli! Anayezishika siku humshikia Bwana; naye asiyezishika hazishiki kwa ajili yake Bwana. Naye anayekula humlia Bwana, kwani humshukuru Mungu. Naye asiyekula hali kwa ajili yake Bwana, maana naye humshukuru Mungu. Kwani kwetu hakuna anayejikalia mwenyewe, wala hakuna anayejifia mwenyewe. Kwani tunapokaa humkalia Bwana, tena tunapokufa humfia Bwana. Basi, ikiwa twakaa au ikiwa twafa, sisi tu wa Bwana. Kwani kwa hiyo Kristo alikufa, akawa mzima tena, apate kuwatawala waliokufa nao wanaoishi.* Lakini wewe unamwumbuaje ndugu yako? Au wewe unambezaje ndugu yako? Kwani sisi sote tutatokezwa mbele ya kiti cha uamuzi cha Mungu. Kwani imeandikwa: Bwana anasema: Kwa hivyo, nilivyo Mwenye uzima, wote watanipigia magoti, nazo ndimi zote zitamwungama Mungu. Basi, kwa hiyo sisi sote kila mmoja atajisemea mwenyewe mbele ya Mungu. Basi, tusiumbuane wenyewe tena, ila mjue, ya kuwa ni kuumbua, mtu akimtegea ndugu yake, ajigonge au ajikwae! Nimeyajua, nikayashika kabisa moyoni kwa kuwa na Bwana Yesu, ya kuwa: hakuna kilicho chenye mwiko hivyo, kilivyo; lakini mtu akikiwazia kuwa chenye mwiko, basi, kwake yeye ni chenye mwiko. Lakini ndugu yako akisikitishwa, wewe ukila, basi, umekwisha kuuacha upendo. Tena ukila usimponze mwenzio, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Yaliyo mema kwenu yaangalieni, yasibezwe! Kwani ufalme wake Mungu sio kula na kunywa, ila wongofu na utengemano na ushangilio unaopatikana katika Roho takatifu. Kwani anayemtumikia Kristo na kuyatenda mambo haya humfalia Mungu, tena hupendwa na watu. Basi, kwa hiyo tukaze kuyafuata mambo yanayopatanisha, ni yaleyale yanayotujenganisha! Usiitengue kazi ya Mungu kwa ajili ya chakula! Kweli, vyote hutakata; lakini mtu akivila na kujikwaa, vimekwisha kumponza. Ni vizuri, usile nyama, wala usinywe pombe, wala usifanye cho chote kinachomkwaza ndugu yako. Wewe unayoyategemea moyoni, yategemee hata mbele ya Mungu! Mwenye shangwe ni yule asiyejipatia hukumu kwa ajili yao yale, aliyoyaona kuwa ya kufaa. Lakini mtu akila mwenye mashaka amekwisha kujipatia hukumu, kwani hakula kwa kumtegemea Mungu. Nayo yote, mtu anayoyafanya pasipo kumtegemea Mungu, ndiyo makosa. Sisi tulio wenye nguvu imetupasa kuyavumilia manyonge yao wenye kukosa nguvu, tusijipendeze wenyewe. Kwetu kila mmoja sharti ampendeze mwenziwe, tusaidiane kujengana vizuri! Kwani naye Kristo hakujipendeza mwenyewe; ila ilikuwa, kama ilivyoandikwa: Masimango yao wanaokusimanga yameniguia mimi. *Kwani yote yaliyoandikwa kale yamendikwa, yatufundishe, tupate kukishika kingojeo chetu tukivumilia, tena tukitulizwa mioyo na yale Maandiko. Naye Mungu mwenye uvumilivu na mwenye kuituliza mioyo ya watu awape, mioyo yenu nyote iwe mmoja tu, kama inavyowapasa walio wa Kristo Yesu! Hivyo mtamtukuza Mungu, Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja. Kwa hiyo mpokeane, kama Kristo alivyotupokea na sisi, Mungu atukuzwe! Kwani nasema: Kristo aliwatumikia waliotahiriwa, ajulishe, ya kuwa Mungu ni mkweli, navyo viagio, baba walivyopewa, akavipatia nguvu. Tena anasema: Wamizimu humtukuza Mungu kwa ajili ya kuhurumiwa, kama ilivyoandikwa: Kwa hiyo nitakuungama kwenye wamizimu, nalo Jina lako na niliimbie. Tena anasema: Furahini, enye wamizimu, pamoja nao walio ukoo wake! Na tena: Mshangilieni Bwana, ninyi wamizimu wote, makabila yote ya watu yamsifu! Tena Yesaya anasema: Shinani mwa Isai ataondokea mwenye kuwatawala wamizimu; huyo ndiye, wamizimu watakayemngojea. Naye Mungu, mnayemngojea, awajaze ninyi nyote furaha na utengemano kwa hivyo, mnavyomtegemea, kingojeo chenu kiongezwe nguvu itokayo kwa Roho Mtakatifu!* Nami mwenyewe, ndugu zangu, nayashika moyoni, kama yalivyo kweli, ya kuwa mema yenu ninyi ni mengi, tena utambuzi wenu ni mwingi, mkaweza hata kuonyana wenyewe. Kwa hiyo nimejipa moyo wa kuwaandikia neno mojamoja na kutokeza maana kama mtu anayewakumbusha. Kwani hiki ndicho kipaji changu, nilichogawiwa na Mungu, nimtumikie Kristo Yesu nikiwatangazia wamizimu Utume mtakatifu wa Mungu na kuwaombea, kusudi wawe kipaji cha tambiko kipendezekacho, kwa kuwa kimetakaswa katika Roho Mtakatifu. Basi, kwa hivyo, ninavyoshikamana na Kristo Yesu, ninaweza kujivunia kazi zake Mungu. Kwani sitajipa moyo wa kusema neno au tendo lo lote, asilolitenda Kristo hapo, nilipoleta wamizimu, wapate kumtii; kwani nguvu iliyowashinda ilikuwa ya vielekezo na ya vioja vyake, tena ile ya Roho takatifu. Hivyo nimeutangaza Utume mwema wa Kristo po pote, nikaanza Yerusalemu, nikaifikisha hata Iliriko na kuzieneza nchi zote zilizoko pembenipembeni. Nikajitunukia, nisiipige hiyo mbiu njema mahali, Kristo alipokwisha kutangazwa, maana nisiujengee msingi wa mtu mwingine, ila yawe, kama yalivyoandikwa: Watakaomwona ndio wasioambiwa Neno lake nao wasiolisikia watalijua maana. Kwa ajili hiyo nalizuiliwa mara nyingi kuja kwenu. Lakini sasa katika nchi za upande huu hakuna, nilikosaza, tena tangu miaka mingi ninatunukia, nije kwenu; nitawafikia hapo, nitakapokwenda Spania. Kwani natazamia kuonana nanyi, nitakapopita, nisindikizwe nanyi kwenda huko; lakini kwanza tupeane kikomo cha maneno na kufurahishana kitambo. Lakini sasa ninakwenda Yerusalemu, niwatumikie watakatifu. Kwani Wamakedonia na Waakea wamependezwa kuchanga machango ya kuwasaidia watakatifu walio maskini huko Yerusalemu. Nao walichanga kwa kupendezwa, tena ndio wadeni wao. Maana wamizimu wakigawiwa nao mali za Kiroho, imewapasa nao kuwatumikia hao na kuwagawia mali za kimtu. Basi, nitakapolimaliza jambo hilo, nikiwapa pato hilo na kulishuhudia, nitaondoka kwenda Spania na kupitia kwenu. Nami najua, ya kuwa nitakapokuja kwenu nitakuja mwenye mema yote, Kristo anayotupa. Lakini ndugu, nawahimiza kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo na kwa hivyo, tunavyopendana Rohoni, mnipiganie na kuniombea kwa Mungu, nipate kupona katika wale wasiotii huko Yudea, tena huu utumishi wangu upendezeke kwao watakatifu huko Yerusalemu, nami nipate kuja kwenu na kufurahi, tupatiane vituo, Mungu akitaka. Naye Mungu mwenye utengemano awe pamoja nanyi nyote! Amin. Nawaagiziani ndugu yetu Febe aliye mtumishi mke wa wateule wa Kenkerea, mmpokee katika Bwana, kama iwapasavyo watakatifu, tena mmsaidie jambo lo lote, atakalopaswa nanyi. Kwani mwenyewe alitunza wengi, hata mimi. Nisalimieni Puriska na Akila waliofanya kazi ya Kristo Yesu pamoja nami! Hao walijitoa wenyewe, wakatwe vichwa, nisiuawe mimi. Mwenye kuwashukuru si mimi peke yangu, ila hata wateule wote walioko kwenye wamizimu. Nisalimieni hata wateule waliomo nyumbani mwao! Nisalimieni mpenzi wangu Epeneto! Ndiye aliyeanza kumtegemea Kristo katika Asia. Nisalimieni Maria aliyetusumbukia sana! Nisalimieni ndugu zangu Andoroniko na Yunia waliokuwa wamefungwa pamoja nami! Nao ni waelekevu machoni pa mitume, tena walinitangulia kumtegemea Kristo. Nisalimieni Ampuliato aliye mpenzi wangu katika Bwana! Nisalimieni Urbano, mwenzetu wa kazi katika Kristo, na mpenzi wangu Staki! Nisalimieni Apele aliyejulikana kuwa Mkristo wa kweli! Nisalimieni wale wa Aristobulo! Nisalimieni ndugu yangu Herodio! Nisalimieni wale wa Narkiso wanaomkalia Bwana! Nisalimieni Tirifena na Tirifosa wanaosumbuka kwa ajili ya Bwana! Nisalimieni mpendwa Persisi kwa kuwa mwanamke aliyesumbuka sana kwa ajili ya Bwana! Nisalimieni Rufo aliyechaguliwa na Bwana, naye mama yake aliye hata mama yangu! Nisalimieni Asinkrito na Fulego na Herme na Patiroba na Herma na ndugu walio pamoja nao! Nisalimieni Filologo na Yulia na Neri na dada yake na Olimpa nao watakatifu wote walio pamoja nao! Msalimiane ninyi kwa ninyi na kunoneana, kama watakatifu wanavyozoea! Wateule wote wa Kristo wanawasalimu. Lakini nawahimiza, ndugu, mwakague wenye matata na makwazo! Hawaushiki ufundisho, mliofundishwa, mwaepuke na kuwaacha! Kwani watu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, ila huyatumikia matumbo yao wenyewe. Nao kwa maneno yao yaliyo mazuri na matamu mno huidanganya mioyo yao wale wasiojua ujanja. Kwani usikivu wenu umejulikana kwa watu wote; hivyo ninawafurahia. Lakini nataka, mwe werevu wa kweli, mambo yenu yawe mema, tena mwe wachanga wasioingia maovu. Naye Mungu mwenye utengemano atamponda Satani miguuni penu upesi. Upole wa Bwana wetu Yesu uwakalie ninyi! Wanaowasalimu ninyi ni Timoteo aliye mwenzangu wa kazi na Lukio na Yasoni na Sosipatiro walio ndugu zangu. Mimi Tertio niliyeiandika barua hii nami ninawasalimu ninyi kwa hivyo, ninavyomkalia Bwana. Anawasalimu Gayo aliye mwenyeji wangu mimi na mwenyeji wa wateule wote. Naye Erasto aliye mshika mali za mji na ndugu Kwarto wanawasalimu. Upole wa Bwana wetu Yesu Kristo uwakalie ninyi nyote! Amin. Mungu ndiye anayeweza kuwashikiza ninyi kwa nguvu ya Utume mwema wa Yesu Kristo, ninaoutangaza, kwani nimefumbuliwa mambo ya fumbo yasiyosemwa kale na kale. Yayo hayo yamefumbuliwa sasa na Maandiko ya Wafumbuaji kwa agizo lake Mungu, mwenye kuwapo kale na kale, wamizimu wote wafunzwe huo usikivu wa kumtegemea. Yeye Mungu aliye peke yake mwenye werevu wa kweli atukuzwe kwa ajili ya Yesu Kristo kale na kale pasipo mwisho! Amin. Mimi Paulo niliyeitwa kuwa mtume wa Kristo Yesu kwa hayo, Mungu ayatakayo, na ndugu Sostene tunawaandikia ninyi wateule wa Mungu mlioko Korinto; mlitakaswa na Kristo Yesu, mkaitwa kuwa watakatifu pamoja na wote wanaolitambikia Jina la Bwana wetu Yesu Kristo ko kote, huko kwao nako huku kwetu. Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo! *Nayavumisha siku zote mema yake Mungu, aliyowagawia ninyi, mwe katika Kristo Yesu. Kwa hivyo, mnavyomkalia, mwazipata mali zote zilizomo katika ufundisho na katika utambuzi wote; nao ushuhuda wa Kristo ukapata nguvu kwenu. Kwa sababu hii hakuna gawio, mnalolikosa mkiwa mnangoja, Bwana wetu Yesu Kristo atokee waziwazi. Yeye ndiye atakayewatia nguvu mpaka mwisho, mpate kutokea siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo mkiwa hamnayo ya kuwakamia. Mungu ni mwelekevu aliyewaita kuwa wenziwe Mwana wake Yesu Kristo aliye Bwana wetu.* Lakini nawaonya, ndugu, kwa ajili ya Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, wote mseme mamoja, kwenu kusiwe na matengano, ila nguvu yenu iwe ile ya kutenda moyo mmoja na kutambua neno moja tu. Kwani ndugu zangu, nimeambiwa mambo yenu na wale wa Kloe, ya kuwa kwenu yako magomvi. Nalisema lile la kwamba: Kwenu kila mmoja husema: Mimi wa Paulo! au: Mimi wa Apolo! au: Mimi wa Kefa! au: Mimi wa Kristo! Je? Kristo amegawanyika? Au ni Paulo aliyewambwa msalabani kwa ajili yenu? Au mmebatiziwa jila la Paulo? Namshukuru Mungu, ya kuwa sikubatiza mtu kwenu ila Krispo na Gayo, maana mtu asiseme: Mmebatiziwa jina langu mimi. Kweli naliwabatiza nao wa nyumbani mwa Stefana. Tena sijui, kama yuko mwingine, niliyembatiza. Kwani Kristo hakunituma kubatiza, ila amenituma kuipiga hiyo mbiu njema, lakini si kwa maneno ya ujuzi wa kimtu, msalaba wake Kristo usitenguliwe. Kwani neno la kuwambwa msalabani ndilo la upuzi kwao wanaoangamia, lakini kwetu sisi tunaookolewa ndilo la nguvu ya Mungu. Kwani imendikwa: Nitauangamiza werevu wao walio werevu wa kweli nao utambuzi wao watambuzi. Yuko wapi aliye mwerevu wa kweli? Yuko wapi aliye mwandishi? Yuko wapi aliye mbishi wa siku hizi? Je? Mungu hakuupumbaza werevu wa ulimwengu huu? *Kwani kwa huo werevu wake ulimwengu huu haukumtambua Mungu na werevu wake wa Kimungu ulio wa kweli; kwa hiyo Mungu amependezwa kuwaokoa wenye kumtegemea akiwatangazia mapumbavupumbavu. Kwani Wayuda hutaka vielekezo, nao Wagriki hutafuta werevu ulio wa kweli. Lakini sisi twamtangaza Kristo, alivyowambwa msalabani; ndipo, Wayuda wajikwaliapo, tena ndipo, wamizimu waoneapo mapumbavu tu. Lakini wale walioitwa, Wayuda na Wagriki, kwao twamtangaza Kristo kwamba: Ni nguvu ya Mungu, tena: Ni werevu wa Mungu ulio wa kweli. Kwani yaliyo mapumbavu ya Mungu ndiyo yenye werevu wa kweli kuupita wa watu, nayo yaliyo manyonge ya Mungu ndiyo yenye nguvu kuzipita za watu. Kwani utazameni, ndugu, wito wenu! Hakuna wengi walio werevu wa kimtu; hakuna wengi walio wenye nguvu; hakuna wengi walio wenye macheo. Lakini walio wapumbavu wa ulimwengu huu ndio, Mungu aliowachagua, awatweze walio werevu wa kweli. Tena walio wanyonge wa ulimwengu huu ndio, Mungu aliowachagua, awatweze wenye nguvu. Tena walio wakiwa wa ulimwengu huu nao waliobezwa ndio, Mungu aliowachagua, hata wasiowaziwa kuwa watu, awaumbue wanaotukuzwa kwamba: Ni watu, kusudi mbele ya Mungu mwenye mwili wa kimtu asijivune, hata mmoja. Kwake yeye ndio, mlikotoka ninyi mliomo mwake Kristo Yesu. Huyu ndiye werevu wetu wa Kimungu ulio wa kweli, na wongufu na utakasi na ukombozi. Basi, iwe, kama ilivyoandikwa: Mwenye kujivuna na ajivunie kuwa wa Bwana!* Nami, ndugu, nilipokuja kwenu nalijia kuutangaza ushuhuda wa Mungu; sikuja kuwaambia maneno makuu ya werevu ulio wa kweli. Kwani kwenu sikuwaza werevu mwingine, asipokuwa Yesu Kristo, naye hivyo, alivyowambwa msalabani. Nami nalikaa kwenu mwenye unyonge na woga na matetemeko mengi. Hata nilipowaambia mbiu yangu, sikutumia maneno ya werevu yenye nguvu ya kushinda, ila nimetumia Roho yenye nguvu, kusudi mmtegemee Bwana, ila visiwe kwa kushindwa na werevu wa kimtu, ila kwa kushindwa na nguvu yake Mungu. *Tena yako ya werevu wa kweli; tunawaambia wale wenye kuyatimiza yote. Lakini nayo siyo ya werevu wa ulimwengu huu, wala wa wakuu wa ulimwengu huu walio wenye kufa. Ila yaliyo ya werevu wa Mungu ulio wa kweli ndiyo, tunayoyasema, nayo yalikuwa hayajatokea bado, maana yalikuwa yamefichwa; huko kale, ulimwengu ulipokuwa haujawa bado, Mungu aliyachagua yayo hayo, yatokee sasa kututukuza sisi. Kwao wanaoutawala ulimwengu huu hakuna aliyeyatambua. Maana kama wangaliyatambua, wasingalimwamba msalabani Bwana aliye mwenye utukufu. Ila ilikuwa, kama ilivyoandikwa: Jicho lisiyoyaona, sikio lisiyoyasikia, moyo wa mtu usiyoweza kuyatia mwake, ndiyo, Mungu aliyowaandalia wale wampendao. Lakini sisi Mungu ametufunulia hayo alipotupa Roho wake. Kwani Roho huyapambanua mambo yote, hata vilindi vya Mungu Kwani yuko mtu ayajuaye mambo ya mtu, isipokuwa roho yake yule mtu iliyomo mwake? Vivyo hivyo mambo ya Mungu nayo hakuna ayatambuaye, asipokuwa Roho wake Mungu. Lakini sisi hatukupewa roho ya ulimwengu huu, ila tumepewa Roho iliyotoka kwa Mungu, tupate kuyajua, tuliyogawiwa na Mungu. Nayo ndiyo, tuyasemayo; tena hatuyasemi kwa maneno, tuliyofundishwa na werevu wa kimtu, ila tulifundishwa na Roho; hivyo mambo ya Roho tunayapatia hata maneno ya Roho. Lakini mtu anayeutii moyo wake tu hayafumbui ya Roho wake Mungu; huyawazia kuwa mapumbavu tu, hawezi kuyatambua, kwani hayo sharti yachunguzwe kwa nguvu ya Roho. Lakini mtu anayemtii Roho huyachunguza yote, lakini mwenyewe hakuna, ambaye achunguzwa naye. Maana: Yuko aliyeyatambua mawazo ya Bwana, amjulishe jambo? Lakini sisi tunayo mawazo yake Kristo.* Nami ndugu, sikuweza kusema nanyi, kama m wenye Roho, m wenye miili tu, m vitoto vichanga katika mambo ya Kristo; kwa hivyo nimesema nanyi kitoto. Nimewanyonyesha maziwa, sikuwalisha vyakula vigumu, maana hamjaviweza bado. Lakini hata sasa hamviwezi bado, kwa sababu mngali bado wenye miili tu. Maana ukiwako kwenu wivu na ugomvi, basi, ninyi ham wenye miili tu? Huu mwenendo wenu sio wa kimtu? Maana mmoja akisema: Mimi wa Paulo, na mwingine: Mimi wa Apolo, basi, ninyi ham wa kimtu? Apolo ni nani? Paulo ni nani? Tu watumishi waliowafundisha kumtegemea Bwana, kila mmoja wetu, kama Bwana alivyompa: mimi nilipanda, Apolo akanywesha, lakini Mungu ndiye aliyeotesha. Kwa hiyo apandeye siye, wala anyweshaye siye, ila Mungu aoteshaye ndiye. Lakini apandaye naye anyweshaye sisi tu wamoja, lakini tutapata kila mmoja wake mshahara wa masumbuko yake mwenyewe. Maana sisi tunasaidiana kazi na Mungu, ninyi m shamba lake Mungu, tena m jengo lake Mungu. Kwa werevu wa kweli, niliogawiwa na Mungu, mimi niliweka msingi kama fundi aliye mwenye ubingwa wa jengo; lakini mwingine anajenga juu yake. Lakini kila aangalie, jinsi anavyojenga juu yake! *Kwani hakuna anayeweza kuweka msingi mwingine pasipo ule uliokwisha kuwekwa, ulio Yesu Kristo. Lakini mtu akijenga juu ya msingi huo kama dhahabu au fedha au mawe yenye bei kubwa au miti au nyasi au mabua, basi, kila mtu kazi yake itatokea waziwazi. Siku ile itaipambanua, maana itafunuliwa kwa kuunguzwa na moto; ni ule moto utakaoumbua, kazi ya kila mtu ilivyo. Jengo la mtu, alilolijenga juu yake likikaa, atapokea mshahara wake; kama jengo la mtu linateketea, atapotelewa nalo, lakini mwenyewe ataokolewa, lakini itakuwa kama kuokolewa motoni. Hamjui, ya kuwa ninyi m nyumba ya Mungu, ya kuwa Roho wa Mungu hukaa ndani yenu? Mtu akiiangamiza nyumba yake Mungu, Mungu atamwangamiza yeye. Maana nyumba yake Mungu ni takatifu, ndiyo ninyi. Mtu asijidanganye! Ikiwa mtu wa kwenu anajiwazia kuwa mwenye werevu wa kweli katika ulimwengu huu, sharti apumbae, apate kuwa mwerevu wa kweli! Kwani huo werevu wa ulimwengu huu ni upumbavu kwa Mungu, maana imeandikwa: Wenye ubingwa huwanasa katika werevu wao mbaya. Na tena: Bwana huyatambua mawazo ya wenye werevu kuwa ya bure. Kwa hiyo mtu asijivune kwa wenziwe! Kwa maana yote ni yenu, akiwa Paulo au Apolo, akiwa Kefa, au ukiwa ulimwengu, kukiwa kuishi au kufa, yakiwa yaliyopo au yatakayokuwapo, yote ni yenu. Lakini ninyi m wake Kristo, naye Kristo ni wake Mungu.* *Hivyo kila mtu atuwazie sisi kuwa watumikizi wa Kristo na watunzaji wa mafumbo yake Mungu. Tena kwa watunzaji halitafutwi jingine, ni hili tu, ajulike kuwa mwelekevu. Kwangu mimi si kitu, nikihukumiwa nanyi au na wengine wanaohukumu kimtu; nami mwenyewe sijihukumu, kwani sinacho kibaya, ninachokijua moyoni. Lakini kwa hivyo si mwongofu; ila atakayenihukumu ni Bwana. Kwa hiyo msihukumu neno lo lote siku hizi, mpaka Bwana atakapokuja; yeye ndiye atakayeyatia mwangani yaliyofichwa gizani; tena ndiye atakayeyafumbua waziwazi mawazo ya mioyo. Hapo ndipo, kila mtu atakapoonea sifa yake kwa Mungu.* Ndugu, kwa ajili yenu nimeyasema haya kama mfano wa mimi na Apolo, mpate kujifundishia kwetu sisi, msijikweze kupapita hapo palipoandikwa kwamba: Mtu asijitutumue kuwa mkuu kuliko mwenziwe na kumpunguza mwingine! Je? Yuko anayekupatia wewe macheo zaidi? Unacho kitu gani, usichopewa? Lakini kama umepewa, wajivuniaje, kama hukupewa? Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata mali nyingi, mkatwaa nao ufalme, msiopewa na sisi. Tunataka sana, mwe wafalme, nasi tupate kuwa wafalme wenzenu. Maana naona, ya kuwa Mungu ametuweka sisi mitume kuwa wa mwisho, kama watu wanaopaswa na kuuawa, kwani sisi ndio wanaotazamwa nao wa ulimwengu wote: malaika, hata watu. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi m wenye akili kwa kuwa naye Kristo. Sisi tu wanyonge, ninyi m wanguvu. Ninyi mwatukuzwa, lakini sisi twabezwa. Mpaka saa hii ya sasa maumivu yetu yako, ni haya: njaa na kiu na uchi na mapigo na kukosa kikao; twasumbuka tukifanya kazi na mikono yetu sisi. Tukitukanwa twaombea mema; tukifukuzwa twavumilia; tukisingiziwa twabembeleza. Tumekuwa kama taka za ulimwengu, kama kifusi chao wote hata sasa hivi. Siyaandiki haya, niwatie soni, ila nawaonya kama watoto wangu, ninaowapenda. Kwani ingawa mnao wafunzi maelfu katika Kristo, lakini hamnao baba wengi. Kwani mimi ndiye niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa kuwapigia hiyo mbiu njema. Kwa hiyo nawaonya, mniige mimi. Kwa sababu hii nimemtuma Timoteo kwenu, huyu ni mtoto wangu mpendwa na mwelekevu katika Bwana. Yeye atawakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo, kama ninavyowafundisha wateule wote po pote. Lakini wako wanaojivuna, kwamba mimi siji kwenu. Lakini nitakuja kwenu upesi, Bwana akitaka; ndipo, nitakapozitambua nguvu zao, wanazojivunia, si maneno yao tu. Maana ufalme wa Mungu sio wa kujisemea, ila uko na nguvu. Mnataka nini? Nije kwenu nikishika fimbo, au nije mwenye upendo na roho ya upole? Po pote panasikilika, ya kwamba kwenu uko ugoni; tena ugoni ulio hivyo hata kwa wamizimu hauko, mtu akiwa na mke wa baba yake. Nanyi mnajitutumua, hamkusikitika hata kidogo. Je? Aliyekifanyiza kitendo hicho ameondolewa kati yenu? Hata nisipokuwako kwenu na mwili wangu, lakini moyo uko kwenu. Hivyo, kama niko kwenu, nimekwisha kumhukumu yule aliyekitenda kibaya kilicho hivyo: katika Jina la Bwana Yesu kusanyikeni ninyi na roho yangu pamoja na nguvu ya Bwana wetu Yesu! Kisha yule mtu aliye hivyo mmtoe na kumpa Satani, mwili wake uangamizwe, roho yake ipate kuokoka, siku ile ya Bwana itakapotimia. Majivuno yenu si mema. Hamjui, ya kuwa chachu kidogo hulichachusha donge lote? Iondoeni kabisa ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya kwa hivyo, mlivyo pasipo chachu! *Kwani nasi tumechinjiwa kondoo wetu wa Pasaka, ndiye Kristo. Kwa hiyo tuile sikukuu yetu pasipo chachu ya kale wala chachu yenye uovu na ubaya, tuyapate yale yasiyochachwa, ndiyo mioyo ing'aayo iliyo yenye ukweli.* Naliwaandikia ninyi katika barua yangu kwa kwamba: Msichanganyike na wagoni! Hapo sikuwasema wagoni wa ulimwengu huu au wenye choyo na wanyang'anyi au wenye kutambikia mizimu. Kama vingekuwa hivyo, ingewapasa kutoka ulimwenguni. Lakini hapo nimewaandikia, msichanganyike na mtu aitwaye ndugu, akiwa mgoni au mwenye choyo au mtambikia mizimu au mwenye matusi au mlevi au mnyang'anyi; basi, ndugu aliye hivyo msile naye! Kwani nina jambo gani nao walioko nje, niwaumbue? Nanyi si kazi yenu kuwaumbua hao, mlionao? Walioko nje Mungu ndiye atakayewaumbua. Mwondoeni yule mbaya, atoke katikati yenu ninyi! Inakuwaje, mtu wa kwenu aliye na jambo na mwenziwe akijipa moyo wa kuja kushtaki mbele yao walio wapotovu, asije mbele yao walio watakatifu? Au hamjui, ya kuwa watakatifu watauhukumu ulimwengu? Ikiwa ulimwengu utahukumiwa nanyi, isiwapase kuamulia mambo yaliyo madogo? Hamjui, ya kuwa tutahukumu malaika? Nayo ya huku nchini yasitupase? Mkitaka kushtakiana mambo ya huku nchini, inakuwaje, mkiwaketisha katika kiti cha uamuzi wale wanaobezwa kwa wateule? Haya nayasemea kuwatia soni. Je? Kwenu hakuna hata mmoja mwenye werevu wa kweli awezaye kuamua ndugu na mwenzake? Kwenu sharti ndugu na ndugu washtakiane, kisha wapelekane kwao wasiomtegemea Mungu? Kweli hayo mambo yote ya kushtakiana ninyi kwa ninyi ni kukosa utimilifu. Sababu gani hamtaki kupotolewa? Tena sababu gani hamtaki kunyang'anywa? Lakini ninyi mwapotoana, mwanyang'anyana wenyewe, tena m ndugu! Au hamjui, ya kuwa wapotovu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msipotelewe! Wagoni na watambikia vinyago na wavunja unyumba na walegevu na wenye kulalana na wezi na wenye choyo na walevi na wenye matusi na wanyang'anyi, hao wote hawatautwaa ufalme wa Mungu. Hata kwenu wako walio hivyo. Lakini mmeoshwa, tena mmetakaswa, mkaupata wongofu uliomo katika Jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho ya Mungu wetu. Kwangu mimi hakuna cho chote chenye mwiko, lakini sivyo vyote vifaavyo: kwangu mimi hakuna cho chote chenye mwiko, lakini kitakachonishinda sikitaki kamwe. Vyakula ni vya tumbo, nalo tumbo ni la vyakula; naye Mungu atavitowesha vyote viwili. Lakini mwili sio wa ugoni, ila wa Bwana, yeye Bwana ni mwenye mwili. Mungu alimfufua Bwana, vivyo hivyo atatufufua hata sisi kwa nguvu yake. Hamjui, ya kuwa miili yenu ni viungo vyake Kristo? Je? Nivichukue viungo vyake Kristo, nivigeuze kuwa vya ugoni? La, sivyo! Au hamjui, ya kuwa mwenye kugandamiana na mke mgoni amekwisha kuwa mwili mmoja naye? Maana asema: Hao wawili watakuwa mwili mmoja. Lakini mwenye kugandamiana na Bwana watakuwa roho moja. Ukimbieni ugoni! Kosa lo lote, mtu atakalolifanya, liko nje ya mwili wake, lakini mgoni huukosea mwili wake mwenyewe. Au hamjui, ya kuwa miili yenu ni nyumba yake Roho Mtakatifu awakaliaye? Ndiye, mliyepewa na Mungu, ninyi ham wenye ninyi. Mmenunuliwa pakubwa, kwa hiyo mtukuzeni Mungu miilini na rohoni mwenu! Maana ni yake Mungu. Mambo, mliyoniandikia, nayajibu hivi: Ni vizuri, mtu asipogusa mwanamke. Lakini kwa ajili ya ugoni kila mtu awe na mkewe mwenyewe, hata kila mwanamke awe na mumewe mwenyewe. Mume ampe mkewe yampasayo, naye mke ampe mumewe yayo hayo. Mke siye mwenye mwili wake, ila mumewe; vilevile naye mume siye mwenye mwili wake, ila mkewe. Msinyamane, isipokuwa mmepatana kukaa hivyo kitambo kidogo, mjipatie siku za kufunga na za kuomba. Kisha mwandamane tena, Satani asipate kuwajaribu, kwani hamwezi kuvumilia pasipo kukoma. Haya nayasema, kama ninavyoyatambua mimi, lakini siyo ya kuagiza. Kupenda napenda, watu wote wawepo kama mimi mwenyewe; lakini kila mtu amegawiwa na Mungu kipaji chake yeye, mmoja hivyo, mwenzake hivyo. Lakini wasiooa na wajane nawaambia: Itawafalia, wakikaa kama mimi. Lakini kama hawawezi kujivumiliza, na waoe. Kwani kuoa ndiko kuzuri kuliko kuchomwa na tamaa. Nao waliokwisha oana nawaagiza, tena si mimi, lakini ni Bwana: Mke asiachane na mumewe! Lakini mke akiwa ameachana na mumewe, sharti akae pasipo kuolewa au apatanishwe tena na mumewe! Naye mume asiachane na mkewe! Nao wengine nawaambia mimi, si Bwana: Aliye ndugu akiwa na mke asiyemtegemea Mungu, naye mkewe anapenda kukaa naye, asimwache! Naye mwanamke akiwa na mume asiyemtegemea Mungu, naye mumewe anapenda kukaa naye, asimwache mumewe! Kwa maana mume asiyemtegemea Mungu hutakaswa na mkewe; naye mke asiyemtegemea Mungu hutakaswa naye aliye ndugu. Ikiwa sivyo, watoto wenu wangekuwa wachafu, lakini sasa wametakata. Lakini wale wasiomtegemea Mungu wakitaka kuvunja unyumba, na wauvunje! Hapo aliye ndugu, akiwa mume au akiwa mke, hakuna kifungo tena kinachomzuia; kwani ninyi Mungu amewaitia mapatano. Kwani wajuaje, wewe mke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mume, kama utamwokoa mkeo? Kwa hiyo nasema: Kila mtu avishike, Bwana alivyomgawia, kila mtu aendelee hivyo, alivyokuwa hapo, Mungu alipomwita! Hivyo ndivyo, ninavyoagiza katika wateule wote. Mtu akiitwa alipokwisha kutahiriwa asivifiche! Mtu akiitwa akiwa hajatahiriwa, asitahiriwe! Kule kutahiriwa siko, nako kutotahiriwa siko, ila kuyashika maagizo ya Mungu ndiko. Kila mtu hivyo, alivyokuwa alipoitwa, na akae vivyo hivyo! Kama ulikuwa mtumwa ulipoitwa, usivionee uchungu! Lakini ukiweza kujikomboa jikomboe! Kwani mtumwa aliyeitiwa kuwa wa Bwana amekwisha kukombolewa na Bwana. Vivi hivi mwungwana aliyeitwa ni mtumwa wa Kristo. Mmenunuliwa pakubwa. Msiwe tena watumwa wa watu! Ndugu zangu, kila mtu hivyo, alivyokuwa hapo alipoitwa, sharti akae vivyo hivyo kwa Mungu! Kwa ajili ya wanawali sikupata agizo la Bwana, ninawaambia, ninayoyatambua kwa hivyo, nilivyogawiwa na Bwana kuwa mwelekevu. Nionavyo kuwa vizuri, ni hivi: kwa ajili ya shida hii, tuliyo nayo inamfaa mtu kukaa hivyo, alivyo: ukiwa umejifunga kuwa na mke usitafute kufunguliwa! Usipokuwa umejifunga kuwa na mke usitafute mke! Lakini hata ukioa hukosi, naye mwanamwali akiolewa hakosi. Lakini wafanyao hivyo huipatia miili maumivu, nayo ndiyo, mimi ninayoyataka kuwaponya Lakini nasema hivi, ndugu zangu: Siku zimepunguka. Hapo panaposalia nao wenye wake sharti wawe, kama hawana! Nao wenye kulia wawe kama wasiolia! Nao wenye furaha wawe kama wasiofurahi! Nao wenye kununua wawe, kama hawana kitu! Nao wenye kuvitumia vya ulimwengu huu wawe, kama wanajitumilia bure tu! Kwani ulimwengu huu, jinsi ulivyo sasa, unatoweka. Nataka, msipatwe na masumbuko. Asiyeoa huyasumbukia mambo ya Bwana, apate kumpendeza Bwana. Aliyeoa huyasumbukia mambo ya ulimwenguni, apate kumpendeza mkewe; hivyo amekwisha kugawanyika. Nayo ya mke na ya mwanamwali ni yaleyale: mke asiye na mume naye mwanamwali huyasumbukia mambo ya Bwana, apate kutakata mwilini na rohoni. Lakini mwenye mume huyasumbukia mambo ya ulimwenguni, apate kumpendeza mumewe. Lakini haya nayasema, kwa kuwa yanawafaa; siyasemi, niwategee kitanzi, ila nayasemea kwamba: Yenu yote yaendelee, kama yapasavyo, mfulize kumkalia Bwana pasipo kuzuiliwa. Lakini mtu akiona, ya kama haimfai mwanawe wa kike, akiwa mtu mzima pasipo kuolewa, -nayo hufikia hapohapo-, basi, na afanye, kama atakavyo! Hakosi, na amwoze! Lakini aliyeushikiza moyo wake ukashupaa vizuri, usiteseke, yuko na nguvu ya kuyashinda mapenzi yake mwenyewe; basi, mtu aliye hivyo akijipa moyo wa kumkataza mwanawe wa kike kuolewa, atafanya vizuri. Hivyo amwozaye mwanawe wa kike anafanya vizuri, lakini asiyemwoza mwanawe wa kike anafanya vizuri kumpita yule. Mke yuko na mwiko siku zote za kuishi kwake mumewe; lakini mumewe anapokufa, amefunguliwa kuolewa naye ye yote, ampendaye, ikiwa tu, kama Bwana atakavyo. Lakini vitakavyomfaa kupita hivi ni kukaa hivyo, alivyo. Hivyo ndivyo, nionavyo mimi; lakini najiwazia, ya kwamba nami ninayo Roho ya Mungu. Mambo ya nyama za tambiko twayajua kwamba: Sote tumeyatambua; tena: Utambuzi huleta majivuno, lakini upendo hujenga. Lakini mtu akijiwazia, ya kuwa amekwisha kutambua kitu, basi, yeye hajautambua bado utambuzi upasao. Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo ametambuliwa naye. Kwa ajili ya kula nyama za tambiko tunajua: hakuna, kinyago kifaliacho humu ulimwenguni, tena hakuna aliye Mungu pasipo mmoja. Kweli viko viitwavyo miungu, kama vya mbinguni au vya ulimwenguni, kwa hiyo miungu yao ni mingi nao mabwana zao ni wengi, lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja, ni Baba. Yote yametoka kwake, nasi tu watu wake. Tena Bwana ni mmoja, Yesu Kristo; vyote viliumbwa naye yeye, hata sisi tumeumbwa naye. Lakini sio wote walio wenye utambuzi huu. Kwa hivyo, walivyozoea kutambikia mizimu, hata sasa wako wanaozila zile nyama, zikiwa za tambiko, lakini mioyo yao iliyo minyonge huchafuliwa kwa kujua maana. Tena hakuna, vyakula vinavyotupatia kwake Mungu. Ikiwa tukila, hakuna tunachoongezewa; ikiwa hatuli, hakuna tunachopungukiwa. Mwangalie tu, matumio yenu yasikwaze wanyonge! Maana wewe uliyeyatambua hayo ukikaa hapo, wanapotambikia mizimu, ule nyama machoni pa mwenzio aliye mnyonge kwa kutojua maana vema, je? Hatahimizwa moyoni mwake, mpaka naye azile nyama zile za tambiko? Hivyo kwa ajili ya utambuzi wako mnyonge anaponzwa, naye ni ndugu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Mkiwakosea ndugu hivyo na kuiponza mioyo yao iliyo minyonge kwa kutojua maana vema, basi, mnamkosea Kristo mwenyewe. Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, sitakula nyama kale na kale, maana nisimkwaze ndugu yangu. Je? Mimi sikukombolewa? Mimi si mtume? Mimi sikumwona Bwana wetu Yesu Kristo? Nanyi ham kazi yangu, niliyomfanyizia Bwana? Nisipokuwa mtume wa wengine, lakini ninyi ndimi mtume wenu. Kwani ninyi m muhuri inayoujulisha utume wangu, ya kuwa ni wa Bwana. Makanio yangu kwao wanaoniulizauliza ndiyo haya ya kwamba: Je? Hatuna ruhusa ya kula na ya kunywa yo yote? Hatuna ruhusa pote, tunapokwenda, kuchukua na mke aliye ndugu, kama wanavyofanya mitume wengine na ndugu za Bwana, hata Kefa? Au labda mimi na Barnaba peke yetu hatuna ruhusa ya kuwapo pasipo kazi? Yuko askari aendaye vitani na kujilipa mwenyewe? Yuko mpanda mizabibu asiyekula matunda yao? Au yuko mchunga kundi asiyetumia maziwa ya kundi kuwa kitoweo? Haya nayasema kimtu? Maonyo nayo hayayasemi yayo hayo? Kwani imendikwa katika Maonyo ya Mose: Ng'ombe mwenye kupura ngano usimfunge kinywa! Hapo Mungu anataka kuwapatia ng'ombe? Hapasemi kabisa kwa ajili yetu sisi? Kweli imeandikwa kwa ajili yetu sisi kwa kufaa, mkulima alimie kingojeo, naye mwenye kupura apurie kingojeo cha kugawiwa. Kama sisi tumewapandia ya kutunza roho, ni vikubwa gani, sisi tukivuna yenu ya kutunza miili? Ikiwa wengine wamepata ruhusa ya kula matumio yenu, hayatupasi sisi kuliko wale? Lakini hatukuitumia hiyo nguvu yetu, ila twayavumilia yote, kwamba Utume mwema wa Kristo tusiuzuie kamwe. Hamjui, ya kuwa hao watumikiao Patakatifu hula yatokayo Patakatifu? Nao wachinja ng'ombe za tambiko hugawiwa fungu lao hapo chinjioni? Vivyo hivyo naye Bwana aliwaagiza watangazaji wa Utume mwema, wajilishe huo Utume mwema. Lakini mimi sikuyatumia mambo hayo hata moja. Nami sikuyaandika haya, kwamba yanitimilie hivyo; maana ningependa kufa kuliko kutenguliwa hilo tukuzo langu. Kwani nikiipiga hiyo mbiu njema sinalo la kujivunia, maana nitashurutishwa. Kwani nisipoipiga hiyo mbiu njema ningepatwa na mambo. Kwani nikiyafanya kwa kuyapenda, napata mshahara; lakini nikiyafanya pasipo kupenda, nako ndiko kuutimiza utunzaji niliopewa. Basi, mshahara wangu ndio nini? Ni huu: nautangaza Utume mwema pasipo upato, nisiyatangue matumio yangu yaliyomo katika huo Utume mwema. Maana mimi niliyekombolewa katika utumwa wote nimejigeuza kuwa mtumwa wao wote, kusudi walio wengi niwapate, wanifuate. Kwao walio Wayuda nimekuwa kama Myuda, niwapate Wayuda. Kwao wenye miiko nimekuwa kama mwenzao mwenye miiko, tena miiko sinayo, ni kwamba tu, niwapate wenye miiko nao. Kwao wasiojua maonyo nimekuwa kama mwenzao asiyejua maonyo, tena sipo pasipo Maonyo yake Mungu, kwani nayakalia Maonyo yake Kristo; huko ni kwamba tu, niwapate nao wasiojua maonyo. Kwao walio wanyonge nimekuwa kama mnyonge mwenzao, niwapate walio wanyonge nao. Hivyo wote nimejifananisha nao katika mambo yo yote, nipate po pote wenye kuokoka. Hayo nayafanya yote kwa ajili ya Utume mwema, nami nipate kugawiwa bia yake. *Hamjui: Penye mashindano wote hupiga mbio, lakini atakayepewa tunzo ni mmoja tu? Nanyi pigeni mbio hivyo, kusudi mpewe! Lakini kila aendaye kushindania hujinyima yote; hao hujinyima, wapewe kilemba kiangamiacho, lakini ninyi mjinyime, mpewe kilemba kisichoangamika! Basi, nami napiga mbio hivyo, si kama sijui, ninavyokimbilia; napigana, lakini si kama anayejipigia tu. Ila nauponda mwili wangu, mpaka nguvu zake ziishie kama za mtumwa, maana mimi ninayetangazia wengine nisije kuwa mwenye kutupwa.* *Ndugu, sitaki, ninyi mkose kujua, ya kuwa baba zetu wote walikwenda wakifunikwa na wingu, nao wote walipita baharini. Wote wakabatiziwa Mose walipokuwa winguni na baharini. Tena chakula cha Kiroho, walichokila wote, ni kile kimoja; nacho kinywaji cha Kiroho, walichokinywa wote, ni kile kimoja. Maana walikunywa maji yaliyotoka katika mwamba wa Kiroho uliofuatana nao; nao mwamba huo ni Kristo. Lakini wale wengi Mungu hakupendezwa nao, kwa hiyo walilazwa jangwani. Hayo yalifanyika, tujifunzie mumo humo, sisi tusitende tamaa ya maovu, kama wale walivyokuwa na tamaa. Wala msitambikie kinyago kama wengine wao! Kama ilivyoandikwa: Watu walikalia kula na kunywa, kisha wakainukia kucheza. Tena tusifanye ugoni, kama wengine wao walivyoufanya, wakauawa siku moja watu 23000. Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaangamizwa na nyoka. Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaangamizwa na mwangamizaji. Lakini hayo yote yaliwapata, tujifunzie mumo humo, yakaandikiwa kutuonya sisi tuliofika penye mwisho wa siku. Kwa hiyo: ajiwaziaye kwamba amesimama, aangalie, asianguke! Hamjaingiwa bado na jaribu lo lote linaloipita nguvu ya mtu. Lakini Mungu ni mwelekevu; hatawaacha ninyi, mjaribiwe na mambo yaupitayo uwezo wenu; lakini hapo, mtakapojaribiwa, atawapatia mzungu, mweze kuvumilia.* Kwa hiyo, wenzangu wapendwa, yakimbieni matambiko ya mizimu! Nasema nanyi, kwa kuwa m wenye akili; yatambueni ninyi, niyasemayo! Kinyweo chenye mbaraka, tukibarikicho, hakitupatii bia ya damu yake Kristo? Mkate, tuumegao, hautupatii bia ya mwili wake Kristo? Kwa sababu mkate ni mmoja, nasi tulio wengi tu mwili mmoja, maana sote twagawiwa huo mkate mmoja.* Mwatazame walio Waisiraeli kwa kuzaliwa! Wenye kuzila nyama za tambiko sio wenye bia ya meza ya kutambikia? Basi, nisemeje? Niseme: Nyama ya tambiko ni kitu? Au niseme: Mizimu ni kitu? Siyo, maana wamizimu waitambikia mizimu yao, hawamtambikii Mungu. Nami sitaki, ninyi mwe wenye bia na mizimu. Hamwezi kukinywa kinyweo cha Bwana nacho kinyweo cha mizimu; hamwezi kula mezani pa Bwana na mezani pa mizimu. Au tumchokoze Bwana? Sisi tuko na nguvu kumshinda yeye? Hakuna cho chote chenye mwiko, lakini sivyo vyote vifaavyo; hakuna cho chote chenye mwiko, lakini sivyo vyote vijengavyo. Pasiwe na mtu mwenye kuyatafuta yaliyo yake, sharti ayatafute yaliyo ya mwenziwe! Vyote vinavyouzwa sokoni vileni pasipo kuuliza vitokapo, mioyo isilemewe! Kwani nchi hii ni yake Bwana navyo vyote vilivyomo. Mtu asiyemtegemea Mungu akiwaalika, nanyi mkitaka kwenda, basi, vyote mnavyoandaliwa vileni pasipo kuuliza vitokapo mioyo isilemewe! Lakini akiwaambia: Hii ni nyama ya tambiko, msiile kwa ajili yake yeye aliyewajulisha, tena kwa ajili ya mioyo isiyojua maana, isilemewe! Sisemi hapa moyo wako unaojua maana, ila wa yule mwingine. Maana visivyo vya mwiko kwangu, vitaumbuliwaje na moyo wa mwingine asiye hivyo? Mimi ninapovila kwa kugawiwa, ninabezwaje kwa vile, ninavyovipokea kwa Mungu? Basi, mkila au mkinywa au mkifanya lo lote jingine, yafanyeni yote, yamtukuze Mungu! Jiangalieni, msiwakwaze Wayuda wala Wagriki wala wateule wake Mungu! Kama nami, nawapendeza wote kwa mambo yote, maana siyatafuti yanifaliayo mimi mwenyewe, ila yawafaliayo wale wengi, wapate kuokoka. Niigeni mimi, kama nami ninavyomwiga Kristo! Nawasifu ninyi, ya kuwa mnanikumbuka po pote, mkashikamana nayo maagizo yangu, kama nilivyowaagiza. Lakini nataka, mjue, ya kuwa kichwa cha kila mume ni Kristo, nacho kichwa cha mke ni mume, nacho kichwa cha Kristo ni Mungu. Kila mume akiomba au akifumbua Neno na kuvaa kichwani, hukipatia kichwa chake soni. Lakini kila mke akiomba au akifumbua Neno pasipo kuvaa kichwani, hukipatia kichwa chake soni, maana hujifananisha kuwa mamoja, kama wenye kunyolewa walivyo. Maana mke asipovaa kichwani, naye akatwe nywele! Lakini mke akiona soni ya kukatwa nyuwele au kunyolewa avae kichwani! Maana mume haimpasi kuvaa kichwani, kwani yeye ubwana wake hufanana nao wake Mungu; lakini mke ubwana wake ndio uleule wa mume. Maana walipoumbwa, mume hakutoka katika mke, ila mke alitoka katika mume. Tena mume hakuumbwa kwa ajili ya mke, ila mke aliumbwa kwa ajili ya mume. Kwa hiyo imempasa mke kushurutishwa kuvaa kichwani kwa ajili ya malaika. Kisha wakiwa wa Bwana, hakuna, mke anachokuwa pasipo mume, wala hakuna, mume anachokuwa pasipo mke. Kwani kama mke atokavyo katika mume, vivyo hivyo hata mume huzaliwa na mke; lakini yote hutoka kwake Mungu. Yapambanueni ninyi kwa ninyi, kama inampasa mke kuomba mbele ya Mungu pasipo kuvaa kichwani! Navyo mlivyoumbwa haviwafundishi, ya kuwa mume haimpasi kamwe kuwa na nywele ndefu? Lakini mke akiwa na nywele ndefu, ni pambo lake zuri. Maana amepewa nywele ndefu, ziwe mavazi yake. Lakini kama yuko anayependa mabisho, basi, mazoea kama hayo hayako wala kwetu wala po pote palipo na wateule wa Mungu. Lakini liko neno, sharti niliseme waziwazi, silisifu, ni hili: Hamkutanii mema, ila mabaya. Kwani kwanza nasikia, ya kuwa hapo, mnapokutania wateule na wateule, yako magawanyiko, nami menginemengine nayasadiki. Kwani matengano hayana budi kuwa kwenu, kusudi walio wakweli kwenu waonekane. Ninyi mnapokutania pamoja, siko kukila Chakula cha Bwana. Kwani mnapokula, kila mmoja huanza kunyang'anya chakula chake mwenyewe; kwa hiyo mwingine yuko na njaa, mwingine amelewa. Je, hamna nyumba zenu za kuliamo na kunyweamo? Au mwawabeza wateule wake Mungu mkiwatia soni wasio na kitu? Niwaambieje? Niwasifu? La! Katika hayo siwasifu. *Maana mimi nalipewa na Bwana, niliyowapa nanyi: Bwana Yesu usiku ule, alipotolewa, akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akasema: Twaeni, mle! Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyizeni hivyo, mnikumbuke! Vivyo hivyo akakitwaa nacho kinyweo, walipokwisha kula, akisema: Kinyweo hiki ndicho Agano Jipya katika damu yangu. Fanyizeni hivyo, kila mtakapokinywea, mnikumbuke! Kwani kila mnapoula mkate huu, mkakinywea nacho kinyweo hiki, kutangazeni kufa kwake Bwana, mpaka atakapokuja! Kwa hiyo kila anayejilia tu mkate huo na kujinywea tu kinhweo cha Bwana atajionea mapatilizo ya mwili na damu ya Bwana. Sharti mtu ajichunguze mwenyewe, kisha aule mkate huo, akinywee nacho kinyweo hicho! Maana mwenye kujilia na kujinywea tu hujilia mapatilizo, hujinywea mapatilizo, kwani haupambanui mwili wa Bwana. Kwa hiyo kwenu wako wengi walio wanyonge na wagonjwa, nao waliolala si wachache. Lakini tunapojichunguza wenyewe hatutapatilizwa. Ila tukipatilizwa na Bwana tunaonywa, tusije kuhukumiwa pamoja nao wa ulimwengu huu.* Kwa hiyo, ndugu zangu, mnapokutania kula, sharti mngojane! Mtu akiwa na njaa ale mwake, kwamba msikutanie mapatilizo! Nayo yaliyosalia nitayaagiza nitakapokuja. *Lakini ndugu, sitaki, ninyi mkose kuyajua mambo ya Kiroho. Mnajua: Mlikuwa wamizimu, napo po pote, mlipoongozwa, mlipenda kuyafuata matambiko ya vinyago visivyosema. Kwa hiyo nawatambulisha, ya kuwa hakuna mwenye Roho ya Mungu anayeweza kusema: Yesu na awe ameapizwa! Tena hakuna anayeweza kusema: BWANA NI YESU! asipokuwa na Roho takatifu. Kweli yako mapitano ya magawio, lakini Roho ni yule mmoja. Tena yako mapitano ya utumishi, lakini Bwana ni yule mmoja. Tena yako mapitano ya nguvu, lakini Mungu anayevitia vyote nguvu kwa watu wote ni yule mmoja. Lakini kila mtu hufunuliwa kipaji chake cha Roho, kwa kwamba wote wakionee upato. Kwani mmoja hupewa na Roho kusema ya werevu wa kweli, mwingine kusema ya utambuzi unaopatana na Roho yule yule. Mwingine hupewa kumtegemea Mungu kwa nguvu ya Roho yuleyule, mwingine hupewa magawio ya kuponya wagonjwa kwa nguvu ya Roho yule mmoja. Mwingine hupewa kutenda ya nguvu, mwingine ufumbuaji, mwingine kuyapambanua ya Kiroho, mwingine misemo migeni, mwingine kuieleza ile misemo. Lakini haya yote huyatenda Roho yule mmoja akimgawia kila mmoja, kama anavyopenda.* Kwani ni kama vya mwili: ulio mmoja unavyo viungo vingi; tena viungo vyote vya mwili, ingawa ni vingi, ni mwili mmoja tu; vivyo hivyo naye Kristo. Kwani kwa nguvu ya ile Roho moja tumebatiziwa sisi sote kuwa mwili mmoja, tukiwa Wayuda au Wagriki, tukiwa watumwa au waungwana; nasi sote tulinyweshwa Roho moja. Kwani nao mwili sio kiungo kimoja, ila vingi. Mguu ukisema: Kwa sababu si mkono, mimi si wa mwili, je? Kwa hiyo sio wa mwili? Nalo sikio likisema: Kwa sababu si jicho, mimi si la mwili je? Kwa hiyo silo la mwili? Mwili wote kama ungekuwa jicho, tungesikiaje? Kama wote ungekuwa sikio, tungenusaje? Lakini Mungu ameviweka viungo mwilini kila kimoja hapo, alipokitaka. Lakini vyote kama vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungepatikana wapi? Sasa viungo ni vingi, lakini mwili ni mmoja. Jicho haliwezi kuuambia mkono: Sikutumii; wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: Siwatumii ninyi. Lakini ni hivyo: vile viungo vya mwili, tunavyoviwazia kuwa vinyonge, hatumika kuliko vingine. Navyo, tunavyoviwazia kuwa vyenye soni, hupata heshima kuliko vingine; navyo visivyo vizuri hupambwa kuliko vingine. Maana vile vilivyo vizuri machoni petu havipambwi. Lakini Mungu ameuunganisha mwili, nacho kilichopunguka uzuri akakipatia heshima kuliko vingine. Maana mwilini msiwe na migawanyiko, ila viungo vipatane kutunzana kila kiungo na mwenziwe. Napo kiungo kimoja kinapoumia, basi, viungo vyote huumia pamoja nacho; napo kiungo kimoja kinapotukuzwa, basi, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Lakini ninyi m mwili wake Kristo, tena m viungo kila mmoja mahali pake. Wako, Mungu aliowawekea wateule: kwanza mitume, wa pili wafumbuaji, wa tatu wafunzi, kisha wenye nguvu, kisha wenye magawio ya kuponya wagonjwa nao watumikizi nao wenye kuongoza nao wenye misemo migeni. Wote ni mitume? Wote ni wafumbuaji? Wote ni wafunzi? Wote ni wenye nguvu? Wote huponya wagonjwa? Wote husema misemo migeni? Wote hufumbua? Jikazeni, mpate magawio yapitayo hayo! Nami nitawaonyesha njia iliyo nzuri kuzipita zote. *Ijapo niseme misemo ya kimtu na ya kimalaika, nisipokuwa na upendo, ndimi upatu wenye milio au njuga yenye makelele. Ijapo niwe mwenye ufumbuaji, nikayajua mafumbo yote na utambuzi wote, hata nikawashinda wote kwa kumtegemea Mungu, nikaweza kuhamisha hata vilima, nisipokuwa na upendo, hakuna nilichokuwa. Ijapo niwagawie maskini mali zangu zote, nikautoa nao mwili wangu, uunguzwe na moto, nisipokuwa na upendo, hakuna nifaacho. Upendo ni wenye uvumilivu na upole; upendo haujui wivu. Upendo haujikwezi, wala haujivuni; haukwazi, wala hauyatafuti yaliyo yake, wala hauchukiziki, wala hauyahesabu maovu. Hauyafurahii mapotovu, ila huyafurahia yaliyo ya kweli. Hujitwika yote, huyategemea yote, huyangojea yote, huyavumilia yote. Hapana, upendo unapokomea; kama ni ufumbuaji, utakoma; kama ni misemo, itanyamaza; kama ni utambuzi, utakoma. Kwani tunayoyatambua, ni fungu tu; nayo tunayoyafumbua, ni fungu tu; lakini matimilifu yatakapokuja, yale ya kifungufungu yatakoma. Nilipokuwa mtoto nalisema kitoto, nikayajua ya kitoto, nikayawaza ya kitoto. Lakini hapo nilipokuwa mtu mzima nimeyaacha yale ya kitoto. Maana sasa tunafanana kama tunaona mfano tu wa yale yasiyofumbuka bado; lakini siku ile tutayaona macho kwa macho. Sasa nayatambua fungu tu, lakini siku ile nitayatambua, kama nitakavyokuwa nimetambulika. Sasa kusikokoma ndiko kumtegemea Mungu na kumngojea na kupenda, huku kutatu. Lakini kuliko kukubwa kukupita kwingine ndiko kupenda.* Ukimbilieni upendo! Jikazeni, myapate ya Kiroho, kupita mengine, mweze kufumbua! Kwani mwenye misemo migeni hasemi na watu, ila husema na Mungu. Kwani hapana amsikiaye, ila husema rohoni yasiyojulikana. Lakini mwenye kufumbua husema na watu akiwajenga na kuwaonya na kuwatuliza mioyo. Mwenye misemo migeni hujijenga mwenyewe tu; lakini mwenye kufumbua huwajenga wateule. Nataka, ninyi nyote mseme misemo migeni, lakini kupita hapo nataka, mfumbue. Kwani mwenye kufumbua ni mkubwa kuliko mwenye misemo migeni, isipokuwa aifumbue, wateule wakapata kujengwa. Lakini sasa, ndugu, kama ningekuja kwenu na kusema misemo migeni, ningewafaa nini, nisiposema nanyi nikiifunua au nikiitambulisha au nikiifumbua au nikiifundisha? Hivyo vingekuwa kama vyombo vinavyojililia tu pasipo roho, ikiwa zomari au zeze; milio isipotambulikana, yatajulikanaje yanayopigwa kwa zomari au kwa zeze? Tena ngoma isipolia na kusikilika, yuko nani atakayejitengeneza kwenda penye kondo? Vivyo hivyo nanyi mnaposema misemo migeni isiyojulikana, yale maneno yenu yatatambulikanaje? Kwani mtakuwa kama wanaojisemea tu na kupigia upepo. Misemo humu ulimwenguni ni mingi mno, lakini hakuna hata mmoja usiotambulika. Nisipoijua maana ya msemo, nitakuwa kama mjinga kwake yeye anayeusema, naye asemaye atakuwa mjinga kwangu mimi. Nanyi hivyo, mjikazavyo kuyapata ya Kiroho, yatafuteni yaleyale yanayowajenga wateule, myaenee! Kwa hiyo mwenye misemo migeni aombe, apate hata kuifumbua! Kwani nikiomba kwa ile misemo migeni, roho yangu huomba, lakini mawazo yangu hayamo. Basi, yafaayo ndiyo nini? Niombe rohoni, tena niombe na kuwaza; niimbe rohoni, tena niimbe na kuwaza. Maana ukimtukuza Mungu rohoni, kama yuko asiyeyajua matukuzo yako, atawezaje kuyaitikia na kusema Amin? Maana hajui, unayoyasema. Kweli wewe unatukuza vizuri, lakini mwingine hajengwi. Namtukuza Mungu, ya kuwa naisema ile misemo migeni kuwapita ninyi nyote. Lakini kwenye wateule kusema maneno matano tu na kuyawaza, kwamba niwafundishe hata wengine, kwanipendeza kuliko kusema maneno elfu kumi kwa hiyo misemo migeni. Ndugu, mawazo yenu yasiwe ya kitoto, ila uovu tu mfanane na vitoto vichanga! Lakini mawazo yenu sharti yawe ya watu wazima! Katika Maonyo imeandikwa: Ukoo huu nitasema nao misemo migeni kwa midomo migeni, lakini hata hivyo hawatanisikia; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwa hiyo ile misemo migeni ni kielekezo, lakini si kwao wamtegemeao Bwana, ila kwao wakataao kumtegemea; lakini ufumbuaji nao ni kielekezo, lakini si kwao wakataao kumtegemea, ila kwao wamtegemeao. Kama wateule wote wanakusanyika pamoja, wote wakasema misemo migeni, tena pakiingia watu waliopumbaa au wasiomtegemea Bwana, je? Hawatasema: Mna wazimu? Lakini kama wote wanafumbua, tena pakiingia asiyemtegemea Bwana au aliyepumbaa ataonywa nao wote na kuumbuliwa nao wote. Hapo yaliyofichika moyoni mwake yanapofunuliwa, ndipo, atakapoanguka kifudifudi na kumtambikia Mungu na kuungama: Kweli Mungu yumo mwenu! Ndugu, yafaayo ndiyo nini? Mnapokusanyika, kila mtu kama yuko na wimbo au fundisho au ufunuo au misemo migeni au mafumbuo yao, yote pia sharti yaje kujenga. Mtu akisema misemo migeni, basi, wawe kama wawili au watatu tu, wasipite hapo, nao waseme mmoja mmoja, kisha mmoja aifumbue. Lakini kama hayuko mwenye kufumbua, basi, wanyamaze penye wateule, ila waseme mioyoni na Mungu. Lakini wafumbuaji waseme wawili au watatu, nao wengine wasikilize tu, wayatambue. Lakini kama mwingine anayekaa anafunuliwa neno, wa kwanza na anyamaze. Kwani mwaweza wote kila mmoja kufumbua, wote wapate kujifunza, wao wote waonyeke. Nazo roho za wafumbuaji huwatii wafumbuaji. Kwani Mungu si Mungu wa uvurugo, ila ni Mungu wa utulivu. Kama ilivyo kwa wateule wote waliotakata, wanawake wanyamaze penye wateule! Kwani wao haiwapasi kusema, ila watii, kama Maonyo yanavyosema. Lakini wanapotaka kujifunza neno, na wawaulize waume wao nyumbani! Kwani haifai kabisa, mwanamke akisema penye wateule. Au je? Neno la Mungu limetoka kwenu, au limewafikia ninyi peke yenu tu? Mtu akijiwazia kuwa mfumbuaji au mwenye Roho na ayatambue, ninayowaandikia, ya kuwa yameagizwa na Bwana! Lakini mtu asipoyajua, basi, na akae pasipo kuyajua! Kwa hiyo, ndugu zangu, jikazeni mpate kufumbua, nako kule kusema misemo migeni msikukataze! Lakini myafanye yote, kama ipasavyo, yaendelee vizuri! *Ndugu, nataka kuwatambulisha vena huo Utume mwema, niliowatangazia; ndio, mlioupokea na kuukalia, tena ndio, ambao mnaokolewa nao, ikiwa mmeyashika maneno ya hiyo mbiu njema, niliyowapigia, isipokuwa mmeitegemea bure. Kwani kwanza nimewatolea, niliyoyapokea hata mimi ya kwamba: Kristo alikufa kwa ajili ya makosa yetu, kama alivyoandikiwa; nayo ya kwamba: Alizikwa, akafufuliwa siku ya tatu, kama alivyoandikiwa. Kisha alimtokea Kefa, kisha akawatokea wale kumi na wawili. Kisha akawatokea ndugu waliopita mia tano, walipokuwa pamoja; namo miongoni mwao wengi wako wazima hata sasa, lakini wengine wamelala. Kisha akamtokea Yakobo, kisha mitume wote. Hayo yote yakiisha, akanitokea hata mimi, ijapo sikuzaliwa, siku zilipotimia. Kwani mimi ni mdogo kuliko mitume wote, hainipasi kuitwa mtume, kwa sababu naliwafukuza wateule wake Mungu. Lakini ni gawio la Mungu nikiwa hivyo, nilivyo, nalo gawio lake, nililopewa, halikuwa la bure; ila nimejisumbua kuwapita wao wote, lakini si mimi, ila ni gawio lake Mungu lililofuatana nami.* Basi, nikiwa mimi, au wakiwa wale, hivyo ndivyo, tunavyovitangaza, tena ndivyo, mlivyovitegemea. *Lakini Kristo akitangazwa, ya kuwa amefufuka katika wafu, kwenu wengine husemaje: Hakuna ufufuko wa wafu? Kama hakuna ufufuko wa wafu, hata Kristo hakufufuka. Lakini kama Kristo hakufufuka, matangazo yetu ni ya bure, nako kumtegemea kwenu ni kwa bure. Tena sisi tungeonekana kuwa mashahidi wa Mungu wa uwongo, kwa sababu tulimshuhudia Mungu, ya kuwa alimfufua Kristo, asiyemfufua, ikiwa watu hawafufuki. Kwani kama wafu hawafufuki, hata Kristo hakufufuka. Lakini kama Kristo hakufufuka, kumtegemea kwenu ni kwa bure, nayo makosa yenu mkingali mnayo bado. Basi, nao waliolala katika Kristo wangekuwa wamepotea. Vikiwa hivyo, nasi katika maisha yetu ya huku nchini, kama kingojeao chetu ni Kristo tu, tungekuwa wakiwa kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amekwisha fufuka katika wafu, ni limbuko lao waliolala.* Kwani kama kufa kulivyoletwa na mtu, vivyo hivyo hata kufufuka kwa wafu kuliletwa na mtu. Kwani kama wanavyokufa wote kwa kuwa wana wa Adamu, vivyo hivyo wote watarudishwa uzimani kwa kuwa wake Kristo, lakini kila mmoja mahali pake: limbuko ndio Kristo; pafuatana walio wake Kristo hapo, atakapojia; mwisho ni hapo, atakapompa Mungu Baba ufalme, ni hapo, atakapokuwa amekwisha kuutangua ukubwa wote na nguvu na uwezo wote. Kwani yeye sharti ashike ufalme, mpaka awaweke adui zake wote chini miguuni pake. Adui wa mwisho atakayeshindwa ni kifo. Kwani aliyaweka yote chini miguuni pake. Lakini pakisemwa: Yote yaliwekwa chini yake, iko waziwazi, ya kuwa ndiyo yote pasipo yule aliyeyaweka yote chini yake. Lakini hapo, yote yatakapokuwa yamekwisha kuwekwa chini yake, ndipo, naye Mwana mwenyewe atajiweka chini yake yule aliyeyaweka yote chini yake. Maana yote yawe yake Mungu po pote. Kama sivyo, wale wanaobatizwa kwa ajili ya wafu wangewapatia nini? Kama wafu hawafufuki kamwe, hubatizwaje? Nasi tunajiponzaje saa zo zote? Ndugu, ninakufa siku kwa siku; ndivyo, ninavyotukuzwa kwenu, tena ndivyo, na Bwana wetu Yesu Kristo anavyonitukuza. Kama nimeshindana na nyama wakali kimtu tu huko Efeso, vingenifaliaje? Wafu wasipofufuka, basi: Na tule, na tunywe! Kwani kesho tutakufa! Msipotelewe! Maongezi maovu huangamiza mazoezo mazuri. Levukeni kweli, msikose! Kwani wengi hawamtambui Mungu. Haya nayasemea kuwatia soni ninyi. Lakini labda yuko atakayeuliza: Wafu watafufukaje? Nao watakuja wenye miili gani? Mjinga wee! Unachokipanda, hakirudi uzimani, isipokuwa kife kwanza. Tena ukipanda hupandi mwili utakaokuwapo, ila unapanda kipunje kitupu, ikiwa cha ngano au cha mbegu nyinginyingine. Lakini Mungu hukipa mwili, kama anavyotaka, kila mbegu hupewa mwili wake mwenyewe. Nyama zote si nyama moja tu, ila nyingine ni ya watu, nyingine ni ya ng'ombe, nyingine ni ya ndege, nyingine ni ya samaki. Tena iko miili ya mbinguni na miili ya nchini. Lakini uzuru wao ya mbinguni uko mbali, nao uzuri wao ya nchini uko mbali. Uzuri wa jua uko mbali, nao uzuri wa mwezi uko mbali, nao uzuri wa nyota uko mbali, kwani nazo nyota na nyota zinapitana uzuri. Nao ufufuko wa wafu utakuwa vivyo hivyo. Hupandwa yenye kuoza, hufufuliwa isiyooza. Hupandwa yenye kubezwa, hufufuliwa yenye kutukuzwa. Hupandwa yenye unyonge, hufufuliwa yenye nguvu. Hupandwa miili ya kimtu, hufufuliwa miili ya kiroho. Kama iko miili ya kimtu, nayo ya kiroho iko. Kwani ndivyo, vilivyoandikwa kwamba: Adamu, yule mtu wa kwanza, alipata kuwa mwenye roho ya uzima. Naye Adamu wa mwisho amepata kuwa roho yenye kurudisha uzimani. Lakini mwili wa kiroho sio wa kwanza, ila wa kimtu ndio uliotangulia, kisha kukafuata wa kiroho. Mtu wa kwanza alitoka nchini, ni wa nchini; mtu wa pili alitoka mbinguni. Yule wa nchini alivyo, ndivyo, wa nchini walivyo nao. Naye yule wa mbinguni alivyo, ndivyo, wa mbinguni watakavyokuwa nao. Nasi tulivyokuwa wenye sura ya yule wa nchini, ndivyo, tutakavyokuwa hata wenye sura ya yule wa mbinguni. Ndugu, hili nalisema waziwazi: Yenye nyama na damu haiwezi kuurithi ufalme wa Mungu, wala yenye kuoza haitairithi isiyooza. Tazameni, ninawaambieni neno lililokuwa limefichika siku zote: Hatutalala sisi sote, lakini sote tutageuzwa. Itakuwapo katika kitambo kidogo tu kama cha kufumba jicho tu; ni hapo, baragumu la mwisho litakapolia. Kwani miili hii yenye kuoza sharti ivae isiyooza, nayo yenye kufa sharti ivae isiyokufa. *Lakini hapo, hii miili yenye kuoza itakapovaa isiyooza, nayo yenye kufa itakapovaa isiyokufa, ndipo, litakapokuwapo lile neno lililoandikwa: Kufa kumemezwa, kukashindwa! Wewe kifo, kushinda kwako kuko wapi? Wewe kuzimu, uchungu wako luko wapi? Kwani uchungu wa kufa ndio ukosaji, lakini nguvu ya ukosaji ndiyo Maonyo. Lakini Mungu atukuzwe atupaye kushinda kwa nguvu ya Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa hiyo, ndugu zangu wapendwa, mjishupaze, msitukutike! Jikazeni kuendelea kazini mwa Bwana po pote, kwa kuwa mmejua, ya kama masumbuko yenu, mnayoyaona kwa ajili ya Bwana, siyo ya bure!* Lakini kwa ajili ya mchango, watakatifu wanaochangiliwa, fanyeni nanyi, kama nilivyowaagiza wateule wa Galatia! Kila siku ya kwanza ya juma kila mmoja wenu na aweke kwake na kuyalimbika yapatanayo na mapato yake, kisha ayachanganye yote, maana machango yasianzwe hapo, nitakapofika! Lakini ndipo nifike, wale, mtakaowachagua ninyi, nitawatuma na barua, wavipeleke vipaji vyenu Yerusalemu. Lakini vikiwa vingi vya kupasa, niende nami, watakwenda pamoja nami. Lakini nitafika kwenu, nitakapokwisha kupita huko Makedonia. Kwani Makedonia nitapita tu; lakini kwenu, kama vinapatikana, nitakaa, labda nitamaliza kwenu siku za kipupwe, ninyi mpate kunisindikiza huko nitakakokwenda Kwani sasa sitaki kuonana nanyi kwa kupita tu; kwani nangojea, nikae kwenu kitambo cha siku, Bwana akipenda. Lakini huku Efeso nitakaa mpaka sikukuu ya Pentekote. Kwani nimefunguliwa mlango mkubwa, tena kazi inaendelea, ijapo wabishi wawe wengi. Lakini Timoteo atakapofika, mmtazame, akae kwenu pasipo woga! Kwani naye anaifanya kazi ya Bwana kama mimi. Pasiwe anayembeza! Ila msindikizeni na kupatana, afike kwangu! Kwani tunamngojea mimi na ndugu. Lakini kwa ajili ya ndugu yetu Apolo mjue, ya kuwa nimemhimiza mara kwa mara, aje kwenu pamoja na hao ndugu; lakini hakutaka kabisa kwenda sasa. Lakini atakuja, patakapomfalia. Kesheni! Kukalieni kumtegemea Bwana, mwe waume wenye nguvu! Mambo yenu yote yafanywe katika upendano! Ndugu, nitakalo tena, ni hili: mwawajua akina Stefana, ya kuwa ndio malimbuko ya nchi ya Akea, tena wamejitoa wenyewe, waje wawatumikie watakatifu. Kwa hiyo nanyi mwatii walio hivyo na kila aliye mwenzao wa kazi na wa masumbuko! Nimefurahiwa na kuja kwake Stefana na Fortunato na Akaiko, kwani ndio walionifanyizia, ambavyo ninyi hamkuweza kunifanyizia. Kwani wameituliza roho yangu nazo roho zenu. Basi, watambueni walio hivyo! Wateule wote walioko Asia wanawasalimu. Akila na Puriskila pamoja nao wote wanaokusanyika nyumbani mwao wanawasalimu sana, kwa kuwa m wa Bwana. Nao ndugu wote wanawasalimu. Mwamkiane mkinoneana, kama watakatifu walivyozoea! Hii salamu yangu mimi Paulo naiandika kwa mkono wangu. Mtu asiyempenda Bwana na awe ameapizwa! Bwana anakuja. Upole wa Bwana Yesu uwakalie ninyi! Upendo wangu wa kuwapenda ninyi, kwa kuwa m wake Yesu Kristo, uwakalie ninyi nyote! Amin. Mimi Paulo niliye mtume wa Kristo Yesu kwa hayo, Mungu ayatakayo, na ndugu Timoteo tunawaandikia ninyi wateule wa Mungu mlioko Korinto nanyi watakatifu nyote mlioko katika nchi yote ya Akea. Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo! Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Ndiye Baba anayewaonea wote uchungu na Mungu anayeipoza mioyo yao wote. Naye ndiye anayetupoza nasi mioyo katika maumivu yetu yote. Kwa hiyo hata sisi twaweza kuwapoza mioyo wale walio katika maumivu yo yote, tukiwapoza mioyo, kama nasi wenyewe tulivyopozwa mioyo na Mungu. Kwani hivyo tunavyofuliza kuteseka, kama Kristo alivyoteseka, vivyo hivyo tunafuliza kupozwa mioyo yetu naye Kristo. Ikiwa tunaumizwa, ni kwa kwamba: Ninyi mpate kupozwa mioyo na kuokoka; ikiwa tunapozwa mioyo, ni kwa kwamba: Ninyi mpozwe mioyo, mwipate ile nguvu inayoonekana hapo, mnapoyavumilia mateso yaleyale, tunayoteswa nasi. Navyo, tunavyongojea kwa ajili yenu, vina nguvu, kwani tumejua: kama mlivyogawiwa mateso, vivyo hivyo mtagawiwa nao upozi wa mioyo. Kwani hatutaki, ndugu, mkose kuyajua mambo ya maumivu yetu yaliyotupata huko Asia, ya kuwa tulilemewa nayo, yakituumiza kuzipita nguvu zetu, tukapotelewa kwamba: Hatutapona. Tukawa tumekata wenyewe mioyoni mwetu kwamba: Sisi tu watu wa kufa tu; tukakataa kujishikiza wenyewe, tupate kushikizwa naye Mungu anayewafufua wafu. Yeye aliyetuponya kufa kulikokuwa hivyo hataacha kutuponya tena; kwa hiyo tunamngojea kwamba: Atafuliza kutuponya vivyo hivyo. Humo hata ninyi mwatusaidia mkituombea; maana wakiwa wengi wanaotutazama, nayo matukuzo yatatoka mioyoni mwa wengi kwa ajili ya kipaji, nilichogawiwa kwa kuombewa nao wengi. Kwani majivuno yetu ndio ushahidi wa mioyo yetu inayoyajua ya kwamba: Tumeendelea ulimwenguni kuwa wenye utakatifu wa kweli wa Kimungu; huu hautoki penye werevu wa kimtu, ijapo uwe wa kweli, ila tumegawiwa naye Mungu; nako kwenu tumejikaza kuwa hivyo. Kwani hatuwaandikii menginemengine, ni yaleyale, mnayoyasoma na kuyatambua. Nami natumaini, ya kuwa mtayatambua maana pasipo kusaza, kama mlivyotutambua na sisi mafungufungu; kwani majivuno yenu ni sisi, kama ninyi mtakavyokuwa majivuno yetu siku ile ya Bwana wetu Yesu. Kwa kushikizwa hivyo moyoni, nalitaka kufika kwenu hapo kwanza, ninyi mpate kuamkiwa mara mbili: hapo, nikipita kwenu kwenda Makedonia, tena nikitoka Makedonia kuja kwenu ninyi, nipate kusindikizwa nanyi, kwenda Yudea. Basi, nilipotaka hivyo, je? Nalijitakia juujuu tu? Au, nayatakayo, nayataka kimtu? Nikisema: Ndio, sharti iwe ndio? Au nikisema: Sio, sharti iwe sio? Lakini Mungu ni mwelekevu, amejua ya kuwa: Neno letu, tulilowaambia, halina maana mbili: kuitikia na kukataa. Kwani Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, aliyetangazwa kwenu na sisi, mimi na Silwano na Timoteo, hakuwa mwenye kuitikia na kukataa, ila mwake yeye mlikuwa kuitikia tu. Kwani viagio vyote vya Mungu vilivyoko vimeitikiwa naye, kisha vimetimizwa naye, Mungu apate kutukuzwa nasi. Lakini Mungu ndiye anayetutia nguvu sisi pamoja na ninyi, tuungane na Kristo; tena ndiye aliyetupatia cheo sisi na kututia muhuri alipotupa Roho, akae mioyoni mwetu, awe rehani yetu. Mimi namtaja Mungu, aushuhudie moyo wangu ya kuwa: Sujaja tena Korinto, nipate kuwajia mwenye upole. Hatujiwazii kuwa mabwana wa kuwaagiza tu, mtakayoyategemea kwenu, ila sisi tu wenzenu wa kusaidiana nanyi, tupate kufurahi pamoja. Kwani mngaliko mkimtegemea Mungu! Lakini moyoni naliwaza hivi: Nisije tena kwenu mwenye sikitiko! Kwani mimi nikiwasikitisha ninyi, yuko nani atakayenichangamsha, asipokuwa yule aliyesikitishwa nami? Kwa sababu hii naliyaandika yale ya kwamba: Nitakapokuja nisisikitishwe nanyi mliopaswa na kunifurahisha; kwa maana ninyi nyote mmenipa moyo wa kwamba: Furaha yangu ni furaha yenu nyote. Kwani naliwaandikia kwa maumivu mengi, moyo ukanipotelea, vikanitoa machozi mengi, siko kwamba msikitishwe, ila mpate kuutambua upendo unaonikaza kuwapenda ninyi kuliko wengine. Lakini kama yuko aliyesikitisha, hakunisikitisha mimi; ila fungufungu, maana nisiseme na kuyapita ya kweli, amewasikitisha ninyi nyote. Aliye hivyo inamtosha, akionywa hivyo na wenzake walio wengi. Kisha imewapasa ninyi kumwendea kwa upole na kumtuliza moyo, asididimizwe, masikitiko yakimshinda. Kwa hiyo nawabembeleza ninyi, mmwonyeshe, ya kuwa mwampenda. Kwani kwa hiyo naliwaandikia, nipate kuutambua welekevu wenu, kama mnatii katika mambo yote. Lakini mmwachiliaye neno, hata mimi humwachilia. Kwamba hata mimi, ikiwa nimemwachilia mtu neno, nimemwachilia kwa ajili yenu machoni pa Kristo, maana tusidanganywe na Satani; kwani mizungu yake hatukosi kuijua. Hapo, nilipofika Tiroa kuutangaza Utume mwema wa Kristo, nikafunguliwa mlango kwa nguvu ya Bwana; lakini sikuona utulivu moyoni mwangu, kwa kuwa sikumkuta ndugu yangu Tito; kwa hiyo nikaagana nao, nikatoka kwenda Makedonia. Lakini Mungu atukuzwe anayetupa kushinda siku zote, tukiwa katika Kristo! Kwa hivyo, tunavyomtumikia yeye, hutokeza po pote waziwazi, ya kuwa wenye kumtambua wafanana na maua yanukayo vizuri. Kwani tukawa mbele yake Mungu kama manukato mazuri ya Kristo kwao wanaookoka, nako kwao wanaoangamia: hao tunawanukia kama wenye kutoka kufani wanaorudi kufani, lakini wale tunawanukia kama wenye kutoka uzimani wanaorudi uzimani. Yuko nani atakayeyaweza hayo. Kwani sisi hatufanani nao wale wengi wanaolichuuzia Neno la Mungu, ila kwa ung'avu wa mioyo, tulioupata kwa Mungu, tunasema kama watu walio pamoja na Kristo mbele yake Mungu. Je? Tunaanza tena kujisifu wenyewe? Au tunatumia kama wengine barua za kusifiwa za kuwapelekea au za kupewa nanyi? Ninyi m barua yetu iliyoandikwa mioyoni mwetu, inatambulikana, maana inasomwa nao watu wote. Vyajulikana, ya kuwa m barua ya Kristo iliyotungwa na sisi, tulipowatumikia; haikuandikwa kwa wino, ila kwa Roho ya Mungu aliye Mwenye uzima; tena haikuandikwa katika vibao vya mawe, ila katika vibao vilivyo mioyo ya watu. *Lakini Kristo ndiye aliyetupa shikizo kama hili kwake Mungu. Huku siko kwamba: Twafaa kuwaza neno lo lote kwa kulitoa mioyoni mwetu; kama liko, tuliwezalo, tutagawiwa na Mungu. Naye ndiye aliyetupa kuwa watumishi wafaao wa Agano Jipya lisilo la andiko, ila la Roho. Kwani andiko huua, lakini Roho hutupatia uzima. Nao utumishi wa mambo yenye kuua, yaliyokuwa yameandikwa na kuchorwa maweni, ulikuwa na utukufu wake, ukawazuia wana wa Isiraeli kuutazama uso wake Mose kwa ajili ya utukufu wa uso wake uliokuwa wa kutoweka tena. Je? Utumishi wa Roho hautakuwa na utukufu kuupita ule? Kwani utumishi utupatiao hukumu ukiwa na utukufu, utumishi utupatiao wongofu utakuwa na utukufu ulio mkuu zaidi kuliko ule.* Kwani utukufu ule uliokuwa wa kifungufungu tu tukiufananisha na utukufu huu uzidio kabisa tutasema: Ule sio utukufu! Kwani chenye kutoweka kikiwa na utukufu, chenye kuwapo kitakuwa na utukufu uupitao ule. *Kwa kuwa wenye kingojeo kama hiki sisi hutumia mioyo isiyojua woga kamwe. Nasi hatufanyi kama Mose aliyeufunika uso wake kwa mharuma, wana wa Isiraeli wasipate kuutazama mwisho wa yale yaliyo yenye kutoweka. Lakini mawazo yao yakashupazwa. Kwani mpaka siku ya leo wakilisoma Agano la Kale, liko limefunikwa vivyo hivyo, lisiwafunukie kwamba: Limetimilia katika Kristo. Ila mpaka leo mioyo yao iko imefunikwa, Mose akisomwa. Lakini hapo, watakapomgeukia Bwana, ndipo, kile kifuniko kitakapoondolewa. Naye Bwana ndiye Roho; napo, Roho ya Bwana ilipo, ndipo, vyote vinapofunguliwa. Lakini nasi sote tunautazama utukufu wa Bwana kwa macho yasiyofunikwa, kama twauona katika kioo; ndivyo, tunavyogeuzwa, tufanane naye, tukipewa utukufu kwa utukufu, tuwe kama watu waliogeuzwa na Bwana mwenyewe aliye Roho.* Kwa sababu tumepewa utumishi huo, nasi kwa hivyo, tulivyohurumiwa, hatuchoki; tukayakataa mambo ya kufichaficha, maana ni yenye soni, kwani hatuendelei kwa werevu mbaya, wala hatuchanganyi Neno la Mungu na uwongo. Ila kwa hivyo, tunavyoyafumbua yaliyo ya kweli, twajitokeza waziwazi mioyoni mwa watu wote, wajue, ya kuwa tupo machoni pa Mungu. *Lakini Utume wetu mwema ukiwa umefunikwa, uko umefunikwa kwao walio wenye kuangamia; maana kwao ndiko, mungu wa nchini alikopofusha mawazo yao wasiomtegemea Mungu, wasiangazwe na mwangaza wa Utume mwema wa utukufu wake Kristo aliye mfano wa Mungu. Kwani hatujitangazi sisi wenyewe, ila twatangaza kwamba: Kristo Yesu ni Bwana, nasi tu watumwa wenu kwa ajili ya Yesu. Kwani Mungu aliyesema: Penye giza pamulike mwanga! ndiye aliyeiangaza mioyo yetu, ndani yao utokee mwanga unaotambulisha hata wengine utukufu wa Mungu uliopo usoni pake Kristo.* Hiki kilimbiko chetu tunacho, lakini kimo katika vyombo vya udongo, kusudi zile nguvu nyingi zilizomo zijulike kwamba: Ndizo zake Mungu, kwamba: Hazotoki kwetu sisi. Po pote twaumizwa, lakini hatusongeki; twahangaishwa, lakini hatuhangaikiki, twakimbizwa, lakini hatuachwi peke yetu; twaangushwa chini, lakini hatuangamiki. Po pote, tunapozunguka, twakujulisha kuuawa kwake Yesu miilini mwetu, kwamba nako kuishi kwake Yesu kupate kutokea miilini mwetu. Kwani sisi tunaoishi hutolewa kila siku, tuuawe kwa ajili ya Yesu kwamba: Nako kuishi kwake Yesu kupate kutokea katika miili yetu iliyo yenye kufa. Kwa hivyo kufa hupata nguvu mwetu, nako kuishi mwenu. Lakini tulivyo wenye Roho yule yule wa kumtegemea Mungu, hutimia kwetu lililoandikwa la kwamba: Nilikuwa nimemtegemea Mungu, kwa hiyo nilisema. Nasi tunamtegemea Mungu, kwa hiyo husema. Kwani twajua: Aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua hata sisi pamoja na Yesu, kisha atatuweka mahali, tutakapokuwa pamoja nanyi. Kwani yote hutupata kwa ajili yenu, maana wenye kugawiwa kipaji wakiwa wengi, hao wengi nao watakazana kuutukuza utukufu wake Mungu. Kwa hiyo hatuchoki, maana ikiwa miili yetu huchakaa, mioyo yetu hupata upya siku kwa siku. Kwani maumivu yetu yaliyo ya sasa hivi tu, yapitayo upesi, huzidi kutupatia utukufu usiopimika, usio na mwisho, tusipoyatazama yaonekanayo, ila yale yasiyoonekana. Kwani yaonekanayo hukaa siku chache tu, lakini yasiyoonekana ni ya kale na kale. Kwani twajua, ya kuwa hivi vijumba vyetu, tupangamo nchini, vitakapobomolewa, tunayo majengo yaliyojengwa na Mungu, ni nyumba zisizojengwa na mikono ya watu, nazo hukaa kale na kale huko mbinguni. Kwani hii ndiyo itupigishayo kite, tukitunukia, tuvikwe makao yetu yatokayo mbinguni; maana tukiwa tumeyavika hatutaonekana kuwa wenye uchi. Kwani sisi tuliomo humu kibandani hupiga kite kwa kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa, ila hutaka kuvikwa, maana iliyo yenye kufa imezwe nayo yenye uzima. Lakini aliyetutengenezea yaya haya ndiye Mungu aliyetupa Roho, awe rehani yetu. Kwa hiyo yako, tunayoyatazamia siku zote tukijua, ya kuwa tukiwa mwetu miilini twamkalia Bwana mbali. Kwani sisi hufanya mwendo kwa kumtegemea Mungu, siko kwa kuona. Lakini kwa hayo, tunayoyatazamia, hupenda sana kuhama miilini, tupate kukaa kwetu kwa Bwana. Kwa sababu hii twajihimiza, tumpendeze yeye, ikiwa tuwe bado mwetu miilini, au tuwe tumekwisha kuitoka.* Kwani sisi sote sharti tutokee mbele ya kiti cha uamuzi cha Kristo, kila mmoja alipwe, aliyoyafanyiza alipokuwa mwilini, yakiwa mema au maovu. Kwa sababu twajua, ya kuwa Bwana huogofya, twawaonya watu, lakini Mungu ndiye, tumtokeaye hivyo, tulivyo. Lakini ninacho kingojeo cha kwamba: Mioyo yenu inajua, ya kuwa nayo tumeitokea hivyo, tulivyo. Hatujisifu tena mbele yenu, ila twataka kuwapa ninyi sababu ya kujivuna kwa ajili yetu, mpate kuwajibu wale wanaojivunia yaliyo machoni tu, yasiyo namo mioyoni. Kwani tulipokuwa kama wenye wazimu, ni kwa ajili ya Mungu; tena tunapoerevuka, ni kwa ajili yenu. *Kwani upendo wa Kristo hutuhimiza sisi, tukawaza hivyo: Mmoja alipokufa kwa ajili yao wote, kwa hiyo wote wamekwisha kufa. Naye alipokufa kwa ajili yao wote alitaka, walio hai wasijikalie wenyewe, ila wamkalie yeye aliyekufa kwa ajili yao, kisha akafufuliwa. Kwa hiyo tangu sasa hakuna, tunayemjua kimwili. Ikiwa tulimtambua Kristo kimwili, sasa hatumtambui tena hivyo. Kwa hiyo mtu akiwa anaye Kristo, amekuwa kiumbe kipya. Yake ya kale yamepita; ukimtazama, yote yamekuwa mapya. Nayo yote hutoka kwa Mungu; ndiye aliyetupatanisha sisi naye yeye, Kristo alipojitoa. Kisha akatupa kuyatumikia hayo mapatano kwamba: Mungu alikuwa katika Kristo, akawapatanisha wa ulimwengu naye yeye, asiwahesabie maanguko yao; akaweka kwetu wenye kuyatangaza hayo mapatano. Hivyo sisi tu wajumbe mahali pake Kristo; ndivyo Mungu mwenyewe anavyowaonya kwa vinywa vyetu sisi. Maana twawabembeleza mahali pa Kristo: Yapokeeni hayo mapatano yake Mungu! Asiyetambua kosa alimgeuza kuwa mwenye makosa kwa ajili yetu, sisi tugeuzwe naye kuwa wenye wongofu wa Kimungu.* *Nasi tulio wenziwe wa kazi twawaonya, msigawiwe bure kipaji cha Mungu. Kwani anasema: Nimekuitikia, siku zilipokuwa za kupendezwa, nikakusaidia siku ya wokovu. Tazameni, siku za kupendezwa kweli ndizo za sasa hivi! Tazameni, leo ni siku ile ya wokovu! Hakuna hata mmoja, tumkwazaye kwa jambo lo lote, utumishi wetu usibezwe. Ila po pote twajitokeza kwamba: Sisi humtumikia Mungu, kwa hivyo twavumilia mengi; maumivu, mahangaiko, masongano, mapigo, mafungo, mashambulio, masumbuko, kukesha na kufunga. Twataka kujijulisha kuwa wenye utakato, utambuzi, uvumilivu, utu, Roho takatifu, upendo usiojua ujanja, neno la kweli, nayo nguvu ya Mungu. Mata yanayotupa kushinda kuumeni na kushotoni ndiyo ya wongofu, ikiwa twatukuzwa, au ikiwa twabezwa; ikiwa twasingiziwa, au ikiwa twashangiliwa. Tuko kama wapotezaji, lakini tu wa kweli; tuko kama wasiojulika, lakini tumetambulikana; tuko kama wenye kufa, lakini tazameni, tu wenye kuishi! Tuko kama wenye kupondwa, lakini hatuuawi; tuko kama wenye kusikitika, lakini twafurahi po pote; tuko kama maskini, lakini twagawia wengi mali nyingi; tuko kama wasio na kitu cho chote, lakini vyote tunavyo.* Enyi Wakorinto, tumewafumbulia vinywa vyetu, tena mioyo yetu nayo imewafungukia kabisa. Humu ndani yetu penu sipo padogo, lakini mioyoni mwenu mnasongeka. Nasema nanyi kama na watoto wangu, nikiwaambia: Tulipeni vivyo hivyo, mkitupatia nasi pakubwa mioyoni mwenu! *Msiingie utumwa wa mwingine pamoja nao wasiomtegemea Mungu! Je? Yako magawio wongufu na upotovu unayoyagawiana? Au iko bia ya mwanga na ya giza? Yako mapatano ya Kristo na ya Beliali? Au liko fungu lililo lake amtegemeaye Mungu nalo lake asiyemtegemea Mungu? Au iko nyumba yake Mungu inayofanana napo penye mizimu? Kwani sisi tu nyumba yake Mungu aliye Mwenye uzima; kama Mungu alivyosema: Nitakaa katikati yao, tena nitatembea katikati yao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa ukoo wangu. Kwa hiyo Bwana anasema: Tokeni kati yao, mjitenge, msiguse yenye uchafu, nami nipate kuwapokea! Ndipo, nitakapokuwa Baba yenu, nanyi mtakuwa wanangu wa kiume na wa kike. Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mwenyezi. Basi, wenzangu, kwa sababu tumepewa viagio kama hivyo, na tujitakase na kuondoa madoa yote ya miili na ya roho! Hivyo tutautimiza utakatifu, maana tutamwogopa Mungu.* Tupatieni kao mioyoni mwenu! Hakuna tuliyempotoa, hakuna tuliyemponza, hakuna tuliyemdanganya. Siyasemei kwamba: Niwapatilize. Kwani nimesema kwanza, ya kuwa mmo mioyoni mwetu, tufe pamoja, kisha tupate kuishi pamoja. *Nikisema nanyi nasema waziwazi kabisa, tena yako mengi yenu, ninayojivunia. Moyo wangu umetulia wote, ukafuliza kuchangamka, hata tukipatwa na maumivu mengi. Kwani tulipofika Makedonia, miili yetu haikuweza kupumzikia kwa ajili ya maumivu yaliyotupata po pote, nje yalikuwako magombano, ndani mahangaiko. Lakini Mungu anayewatuliza wanyenyekevu mioyoni mwao, alitutuliza sisi kwa kuja kwake Tito. Lakini kulikotutuliza siko kuja kwake tu, ila nao utulivu, mwenyewe aliotulizwa nao alipowaona, mlivyo. Naye akatusimulia, mnavyotunukia kutuona, mnavyosikitika, mnavyofanya bidii kwa ajili yangu mimi. Hivi vikanifurahisha kuliko vingine. Nami ikiwa nimewasikitisha na barua yangu sijuti sasa. Na kama nalijuta hapo, nilipoona, ya kuwa ile barua imewasikitisha kitambo, sasa nafurahi, si kwa sababu mmesikitishwa, ila kwa sababu masikitiko, mliyoyapata, yamewafundisha majuto. Kwani mmesikitishwa Kimungu, maana msiponzwe na jambo lo lote litokalo kwetu. Kwani sikitiko la Kimungu humpeleka mtu penye wokovu, likimpatia majuto yasiyojutika tena. Lakini sikitiko la kiulimwengu humpeleka mtu penye kufa.* Kwani tazameni, kule kusikitishwa Kimungu kuko huko ndiko kulikowahimiza hivyo, mjikanie kwa kuona machukivu na woga, mkatunukia kulilipiza lile neno upesi. Mlipoyafanya hayo yote mmejitokeza wenyewe, ya kuwa hammo katika jambo lile. Nami hapo, nilipowaandikia, sikuandika kwa ajili yake aliyepotoa, wala kwa ajili yake aliyepotolewa, ila naliandikia kwamba: Kwenu kuonekane, ninyi mnavyojihimiza kwa ajili yetu mbele ya Mungu. Kwa hiyo tumetulizwa mioyo; na kwa hivyo, mioyo yetu ilivyotulia, furaha yetu ikaongezwa na furaha, Tito aliyokuwa nayo, kwani roho yake imepozwa kwenu po pote. Kama liko jambo la kwenu, nililojivunia kwake, halikunitokeza kuwa mwongo; lakini kama tulivyowaambia nanyi yote yaliyo ya kweli, vivyo hivyo hata yale, tuliyojivunia kwake Tito, yaliyokuwa ya kweli. Ndipo, moyo wake ulipowageukia, ukafuliza kuwapenda, akiwakumbuka, ninyi nyote mlivyomtii, mlivyompokea, woga ukiwatetemesha. Nafurahi, ya kuwa ninaweza kuwatazamia ninyi katika mambo yo yote. Ndugu, twawatambulisha kipaji cha Mungu, wateule wa Makedonia walichogawiwa: maana walipojaribiwa na maumivu yao mengi wameshinda, wakachangamka sana; kwa hiyo hao walio wenye umaskini usiopimika wakajikaza kuonyesha wingi wa mali zilizomo katika mioyo yenye neno moja tu. Kwani nawashuhudia kwamba: Wenyewe walipendezwa na kuchanga, kama walivyoweza, na kupapita hapo, walipoweza. Wakatubembeleza sana na kutuomba, tusiwakataze kulitoa fungu lao la kuingia katika bia hiyo ya kuwatumikia watakatifu. Tena hawakutoa, kama tulivyowangojea, ila kwanza walijitoa wenyewe kumtumikia Bwana na sisi; hivyo wameyamaliza, Mungu ayatakayo. Kwa hiyo tulimhimiza Tito, aitimize hata kwenu kazi hiyo ya vipaji, kama alivyoianza kwanza. Lakini kama mwapitavyo wengine katika mambo yo yote, ikiwa kumtegemea Mungu au kupiga mbiu au kutaka utambuzi au kujihimiza kufanya mema yo yote au kutupenda kwa moyo, kama tunavyowapenda ninyi, hivyo sharti mwapite hata katika vipaji hivi. Sisemi, kwamba niwatolee nguvu, lakini kwa hivyo, wengine walivyojihimiza, nataka, upendo wenu nao utambulike, ya kama ni wa kweli. Kwani mmekitambua kipaji, tulichopewa na Bwana wetu Yesu Kristo: Huyu alikuwa mwenye mali nyingi, akawa maskini kwa ajili yenu, kwamba umaskini wake yeye uwapatie ninyi mali nyingi. Nami niliyoyatambua humu, ndiyo, ninayowatolea, kwani yanawafalia ninyi: mwaka wa jana mlitangulia kuifanya kazi hiyo; tena siko kuifanya tu, mlianza hata kuiitikia. Lakini sasa sharti mmalize kuifanya, maana kama mapenzi yenu ya kuiitikia yalivyotokea upesi, vivyo hivyo mtokeze nayo mapenzi ya kuifanya mkichanga kwa vile, mlivyo navyo. Kwani kama yako mapenzi, mtu hupendezeka akivitoa, alivyo navyo, asivitoe, asivyo navyo. Kwani hatuchangii kwamba: Wengine wapate kutulia, ninyi mkiumizwa, ila sharti yalinganike: mapato mengi yenu yao wale sharti yapunguze makosekano yenu ya siku nyingine; hivyo yatalinganika, kama ilivyoandikwa kwamba: Aliyeokota nyingi hakufurikiwa; wala aliyeokota chache hakupungukiwa. Lakini na tumshukuru Mungu aliyempa Tito kujihimiza vivyo hivyo moyoni mwake kwa ajili yenu. Kwani tulipombembeleza, akaitikia. Lakini kwa hivyo, alivyokaza kujihimiza, aliondoka kwenda kwenu kwa mapenzi yake mwenyewe. Tukatuma pamoja naye ndugu mmoja anayesifiwa kwenye wateule wote hivyo, anavyoutangaza Utume mwema. Lakini sivyo hivyo tu, ila hata kuchaguliwa amechaguliwa nao wateule kuwa mfuasi wetu wa kutusaidia katika kazi hii ya vipaji, tutumikiayo sisi, tumtukuze Bwana, tukijulikana kuwa wenye kumpendeza. Hivyo twajikinga, mtu asitusengenye kwa ajili ya machango haya makubwa yatumikiwayo nasi. Kwani twajilindia, yaendelee vizuri, sipo mbele ya Bwana tu, ila napo mbele ya watu. Tena pamoja nao tulituma ndugu yetu, tuliyemwona mara nyingi katika mambo mengi, anavyojihimiza. Lakini sasa anakaza kujihimiza, kwa sababu yako mengi, anayoyatazamia kwenu. Basi, Tito mwamjua kuwa mwenzangu anayenisaidia kazi za kwenu; nao hao ndugu zetu ni mitume wa wateule, maana wampatia Kristo utukufu. Basi, hao waonyesheni upendo wenu, tuliojivunia tulipowatukuza ninyi! Uonyesheni mbele yao wateule! Kwa ajili ya hayo matumikio yanayochangiwa watakatifu hainipasi kuwaandikia ninyi. Kwani najua, yalivyowapendeza; nami ninajivunia kwa ajili yenu kwa wamakedonia kwamba: Waakea wamejitengeneza tangu mwaka wa jana. Nako kujihimiza kwenu kumehimiza wengine wengi. Lakini nimewatuma hao ndugu, maana hivyo, tulivyojivuna kwa ajili yenu, visipungukiwe katika jambo hili, ila mjulikane, ya kuwa mmejitengeneza, kama nilivyosema. Maana kama Wamakedonia wanakuja pamoja nami, wakawaona ninyi, hamkujitengeneza, tutakuwa waongo sisi, nisiseme: Ninyi, kwa ajili ya hayo majivuno yetu. Kwa hiyo nalijishurutisha kuwaonya ndugu waliotangulia kufika kwenu, waanze kuvichanga vipaji vya upendo wenu, mlivyotuagia kale, tuvikute, vimekwisha kuchangwa kuwa vipaji vya upendo wa kweli, sivyo vya choyo. *Twajua hayo: Mwenye kupanda kwa choyo huvuna yenye choyo; naye mwenye kupanda kwa kubariki huvuna yenye mbaraka. Kila mtu atoe, kama alivyoanza kupima moyoni, asitoe akiwa na mafundo au akishurutishwa! Kwani Mungu humpenda mwenye kutoa na kushangilia. Naye Mungu anaweza kuwapatia matunzo yote, kwamba hayo, mpaswayo nayo, siku zote yawatoshee kabisa, tena yasalie ya kutolea kazi njema zote, kama ilivyoandikwa: Alizimwaga, akawagawia wao waliozikosa; huu wongofu wake hukaa kale na kale. Lakini yeye anayemtolea mpanzi mbegu hutoa nao mkate wa kula; yeye ataziongeza nazo mbegu zenu, ziwe nyingi, kisha atayachipuza mazao ya wongofu wenu. Hivyo mtakuwa wenye mali katika mambo yote, mpate mioyo yenye neno moja tu; hii ndiyo inayomfanyia Mungu kazi na kutupa mikononi vipaji vya kumtukuza.* Kwani kazi hii ya kuchanga vipaji, tunayoitumikia, siyo ya kuyaondoa tu mapungufu ya watakatifu, ila kupita hapo inatimilika kwao wengi, wakimtolea Mungu vipaji vya kumshukuru. Kazi hii, tunayoitumikia, ikijulikana kuwa ya upendo wa kweli, watamtukuza Mungu, maana mmeyatii hayo, mnayoyaungama kuwa Utume mwema wa Kristo, nayo mioyo yenu ikajulika kwao kuwa yenye neno moja tu kwa hivyo, mlivyowagawia hao nao wengine wote. Kwa ajili hii watawaombea ninyi wakitunukia kuwaona, kwa sababu Mungu aliwapa makuu kuliko wengine. Na tumshukuru Mungu, kwani ametupa kipaji kisichowezekana kusimuliwa chote! Nawaonya ninyi kwa upole na kwa utu wa Kristo mimi Paulo mwenyewe niliye mnyenyekevu kwenu nikiwaona, nikawatolea makali nikiwa mbali! Nawaomba, msinishurutishe kuyatumia hayo makali nitakapofika. Mwenyewe nadhani, yafaa kuwaendea na nguvu wale wachache wanaotudhania, ya kwamba sisi huendelea na kufuata tamaa za miili. Kwani hata tunapoendelea katika miili hatujigombei, kama miili itakavyo. Kwani mata ya magombano yetu si ya kimwili, lakini yako na nguvu ya Kimungu, yaweza kubomoa ngome kama hapo, yanaponyenyekeza mawazo yote ya kujikweza na kuuinukia utambuzi wa Mungu, au yanapoteka mawazo yote, yaje kumtii Kristo. Nasi tuko tayari kumlipiza kila mtu asiyetii, hapo mtakapokuwa mmemaliza kutii. Yatazameni yanayoonekana machoni! Mtu akijishikiza kwa kwamba: Ni wa Kristo, na atie hili nalo moyoni la kwamba: Kama yeye alivyo wa Kristo, vivyo hivyo nasi! Ikiwa nafuliza kujivunia nguvu yetu, Bwana aliyotupa, tuwajenge, tusiwajengue, napo hapo sitashindika kuwa mwongo, wala sitafanana na mtu anayewaogopesha tu kwa barua. Kwani wako wanisengenyao kwamba: Barua zake ni ngumu zenye nguvu, lakini akiwapo kwa mwili ni mnyonge, nayo maneno yake hubezeka. Aliye hivyo na alifikiri hili: tunavyovisema kwa barua tusipokuwapo, ndivyo, tutakavyovitimiza tutakapokuwapo. Kwani hatujipi moyo wa kujihesabu au kujifananisha nao walioko, wakijisifu wenyewe. Lakini hao hakuna, wajuacho maana, kwani kipimo chao cha kujipima ndio wenyewe tu, nao mfano wa kujifananisha nao ndio wenyewe tu. Lakini sisi hatutaki kujivuna pasipo kipimo, ila kipimo chetu ni mpaka, Mungu aliotukatia; hivyo tulifika hata kwenu. Kwani hatujitanui wenyewe kama wasiowafikia, maana hata kwenu ni sisi waliotangulia kuwatangazia Utume mwema wa Kristo. Nasi hatuupiti mpaka, tujivunie masumbuko yao wengine, lakini kumtegemea Mungu kutakapokulia kwenu, papo hapo tunangojea mipaka yetu, tuliyowekewa, ikuzwe kuipita ile ya kwenza, tupate kuutangaza Utume mwema hata kwao wakaao mbali kuwapita ninyi. Lakini hatutafuti majivuno tukiingia nchi iliyoisha kupigiwa hiyo mbiu njema na wengine. Lakini mwenye kujivuna na ajivunie kuwa wa Bwana! Kwani anayejisifu mwenyewe siye mkweli, ila yule anayesifiwa na Bwana. Ingefaa, mnivumilie, nikitumia upuzi kidogo; najua, mtanivumilia. Kwani wivu, ninaouona kwa ajili yenu, ni wa Kimungu; maana naliwaposea ninyi mume mmoja, ni Kristo, niwapeleke kwake kuwa mwanamwali mwenye kutakata. Lakini kama nyoka alivyomdanganya Ewa kwa werevu wake mbaya, ninao woga wa kwamba: Vivyo hivyo nayo mawazo yenu yataangamizwa, msiweze tena kuandamana na Kristo peke yake tu na kumng'alia. Kwani mtu anapokuja kwenu na kutangaza Yesu mwingine, tusiyemtangaza sisi, au mnapopata roho nyingine, msiyoipata, au mnapotangaziwa Utume mwema mwingine, msioupokea, basi, ninyi huvumilia vizuri. Lakini nadhani, hakuna nishindwacho nao wale wajipao macheo yote ya utume. Hata nikiwa mpumbavu wa kusema, si mpumbavu wa kutambua, nanyi mmetuona kuwa hivyo po pote katika mambo yote. Au nimekosa, nilipojinyenyekeza, ninyi mpate kuwa wakubwa? Au nimekosa, kwa kuwa nimewatangazia Utume mwema wa Mungu pasipo malipo? Wateule wengine nimewapokonya na kutwaa matunzo, nipate kuwatumikia ninyi. Napo, nilipokuwako kwenu, nikawa nimekosa vyakula, hakuna, niliyemsumbua. Kwani ndugu waliokuja toka Makedonia waliniongezea, nilivyovikosa. Katika mambo yote nimejiangalia, nikae kwenu pasipo kuwasumbua, navyo ndivyo, nitakavyojiangalia. Kwa hivyo ukweli wake Kristo ulivyomo mwangu, hayo majivuno yangu hayatavunjika katika nchi za Akea. Kwa sababu gani? Kwamba siwapendi ninyi? Mungu amevijua! Lakini nifanyalo nitafuliza kulifanya, niiumbue mizungu yao wale wanaotafuta mizungu ya kujivunia kwamba: Sisi tulivyo, nao huonekana kuwa vivyo hivyo. Kwani hao ndio mitume wa uwongo na wafanya kazi wajanja, hujigeuza kuwa mitume wa Kristo. Nalo hili silo la kustaajabu. Kwani Satani mwenyewe hujigeuza kuwa malaika mwenye mwanga. Kwa hiyo si neno kubwa, watumishi wake nao wakijigeuza kuwa watumishi wenye wongofu, lakini mwisho wao utakuwa umepatana na kazi zao. Nasema tena, mtu asiniwazie kuwa mpuzi. Kama hamtaki, vilevile nipokeeni kama mpuzi, nijivune nami kidogo! Ninayoyasema sasa, siyasemi kuwa maneno ya Bwana, ila nayasema kama ya upuzi tu kwa hivyo, tulivyoyafikia majivuno. Kwa sababu wengi hujivuna kimtu, nami nitajivuna. Kwani ninyi mlio wenye akili hupenda kuwavumilia wapuzi. Mwavumilia, mtu akiwafanya watumwa, akiwala, akiyatwaa yaliyo yenu, akijikuza, akiwapiga usoni. Naona soni nikisema: Hayo hatuyawezi, tu wanyonge; lakini jambo lo lote, mtu alilojipa moyo wa kujivunia, (nasema kipuzi) nami najivunia lilo hilo. Ni Waebureo? Hata mimi. Ni Waisiraeli? Hata mimi. Ni uzao wake Aburahamu? Hata mimi. Ni watumishi wa Kristo? Mimi nawapita; nasema kama mwenye wazimu. Nimesumbuka kuwapita, nimefungwa kuwapita, nimepigwa kuwapita kabisa, mara nyingi nimetakiwa kufa. Mara tano nalipata kwa Wayuda fimbo 40 kupungua moja, mara tatu nalipigwa viboko, mara moja nalipigwa mawe, mara tatu chombo changu kimevunjika baharini, nikawamo kilindini usiku na mchana. Safari zangu ni nyingi, nikapata masumbuko ya mito na masumbuko ya wanyang'anyi na masumbuko ya watu wa ukoo wetu na masumbuko ya wamizimu na masumbuko ya mijini na masumbuko ya nyikani na masumbuko ya baharini na masumbuko yaliyoko kwenye ndugu wa uwongo. Nimeumia, mpaka nikachoka, nikikesheshwa mara nyingi, nikiumizwa na njaa na kiu, nikinyimwa mara nyingi vyakula, nikiwekwa penye baridi pasipo nguo. Hayo ya nje hupitwa nayo yanijiayo kila siku, nikiwasumbukia wateule wote. Yuko mnyonge asiyenitia unyonge nami? Yuko anayekwazwa, nisipoumizwa nami? Nikishurutishwa kujivuna nitajivunia unyonge wangu. Mungu, Baba wa Bwana Yesu, atukuzwaye kale na kale anajua: sisemi uwongo. Huko Damasko mtawala watu wa mfalme Areta aliulinda mji wa Damasko, apate kunikamata. Nami nikatolewa dirishani, nikashushwa katika kapu ukutani, nikaokoka mikononi mwake. Nashurutishwa kujivuna, hata isifae kitu. Lakini sasa nitafikia, nilivyotokewa na Bwana, nayo niliyofunuliwa. Yuko mtu nimjuaye kuwa mwenye Kristo; sasa miaka yapata 14, kama alikuwa mwilini, sijui, au kama alikuwa ametengwa na mwili wake, sijui; Mungu anayajua. Mtu huyo alipokonywa na kupelekwa, mpaka aiingie mbingu ya tatu. Nami nimemjua mtu huyo; kama alikuwa mwilini, au kama alikuwa pasipo mwili wake, sijui; Mungu anayajua. Naye alipokonywa kupelekwa Paradiso, akasikia maneno yasiyosemeka, yasiyowezekana kusemwa na mtu. Kwa ajili yake yeye nitajivuna, lakini kwa ajili yangu mimi hakuna, nitakalojivunia, isipokuwa unyonge wangu. Kama ningetaka kujivuna, singekuwa mpuzi, kwani ningesema yaliyo ya kweli. Lakini najikinga, mtu asiniwazie kuwa mkuu kuliko hapo, anionapo na kunisikia. Tena yako mafunuo makuu yote, niliyoyapata; lakini kwa kwamba nisijikweze kwa ajili yao, nimetiwa chomeo mwilini mwangu, ndio mjumbe wake Satani; akafunguliwa, anipige makonde nisijikweze. Kwa ajili yake yeye nimemlalamikia Bwana mara tatu, aniondokee; naye akaniamba: Gawio langu likutoshee! Kwani katika unyonge ndimo, nguvu yangu itimilikamo. Kwa sababu hii kinipendezacho kupita vingine ni kujivunia manyonge yangu, nguvu ya Kristo ipate kunikalia. Kwa hiyo ninaviona kuwa vema, nikiwa mnyonge au nikikorofishwa au nikihangaishwa au nikifukuzwa au nikisongwa kwa kuwa wake Kristo. Kwani ninapokuwa mnyonge, ndipo, nilipo mwenye nguvu.* Nimekuwa mpuzi wa kujivuna, lakini ninyi mmenishurutisha. Kwani ingefaa, mimi nisifiwe nanyi. Kwani hakuna, nishindwacho nao wale wajipao macheo yote ya utume, hata nikiwa si kitu mimi. Yamjulishayo mtu kuwa mtume yamefanyika kati yenu, kama ni uvumilivu mwingi, au kama ni vielekezo na vioja na vya nguvu. Kuna nini, mliyopungukiwa kuliko wateule wengine, isipokuwa hii tu, ya kuwa sikuzila mali zenu ninyi? Niachilieni upotovu huu! Tazameni, mara hii ni ya tatu, nikiwa tayari kuja kwenu, tena sitazila mali zenu. Kwani siyatafuti yaliyo yenu, ila nawatafuta ninyi wenyewe. Kwani haifai, watoto wawawekee wazazi wao vilimbiko, ila wazazi sharti wao wawawekee watoto. Lakini mimi yanipendezayo sana ni kutoa yaliyo yangu, kweli hata mwenyewe nitatolewa kwa ajili yenu ninyi; nikijipingia kuwapenda, itafaa nikipungukiwa kupendwa? Basi, kwa sababu mimi sikuwasumbua, wale husema: Kwa kuwa mwenye werevu mbaya nimewakamata kwa hila. Je? Nimeyatwaa yaliyo yenu ninyi kwa mikono yao wale, niliowatuma kwenu? Nimemwonya Tito, nikatuma pamoja naye yule ndugu. Je? Yako yenu, Tito aliyoyatwaa? Roho ituendeshayo siyo ileile moja? Nazo nyayo, tuzifuatazo, sizo zizo hizo? Mmeanza kale kutuwazia, ya kuwa twajikania mbele yenu. Lakini Mungu ajua: twasema kwa kuwa wake Kristo. Nayo yote tunayasema, tuwajenge ninyi, wapenzi. Maana naogopa, ya kuwa nitakapokuja sitawaona ninyi, kama nitakavyo kuwaona, tena ya kuwa nami hamtaniona nanyi, kama mtakavyo kuniona. Naogopa kukuta magombano na wivu na mifundo ya mioyo na machokozi na masingizio na mateto na majivuno na matukutiko. Kwa hiyo naogopa kwamba: Nitakapofika kwenu, Mungu wangu ataninyenyekeza tena, nami nitapata kusikitika kwa ajili yao wengi waliokosa kale pasipo kuyajutia mambo ya uchafu na ya ugoni na ya uasherati, waliyoyafanyiza. Hii itakuwa mara ya tatu, nikija kwenu. Hapo kila jambo litamalizika kwa kusemewa na mashahidi wawili au watatu. Nimekwisha kusema kale, nilipokuwako kwenu mara ya pili, tena nayasema sasa, nisipokuwako kwenu, kwamba: Waliokosa kale nao wote wengine, hapo, nitakapokuja tena sitawapatia upole. Kwani mwataka kujaribu, kama ni Kristo kweli anayesema kinyuwani mwangu; naye hawaendei kwa unyonge, ila hutenda nguvu kwenu. Kweli amewambwa msalabani kama mnyonge, lakini anaishi kwa nguvu ya Mungu. Nasi ijapo tuwe wanyonge kwa kuwa wake, ninyi mtaona, tutakavyoishi pamoja naye kwa nguvu ya Mungu. Jijaribuni, kama mnakuwa mnamtegemea! Jionyesheni kuwa wakweli! Au hamjitambui wenyewe, kama Yesu Kristo mnaye mwenu? Msipoyajua, ham wa kweli. Lakini nangojea, mtutambue sisi kuwa wenye kweli. Lakini twamwomba Mungu, ninyi msifanye uovu wo wote, siko kwamba sisi tuonekane kuwa wakweli, ila ni kwamba ninyi myafanye yaliyo mazuri, nasi tuwe kama waongo. Kwani hakuna, tunachokiweza tukiyazuia yaliyo ya kweli, ila sisi hujipingia yaliyo ya kweli. Kwani twachangamika, tukiwa wanyonge sisi, ninyi mkiwa wenye nguvu. Nalo hili ndilo, tuliombalo: ninyi mtengenezeke! Sasa nisipokuwako kwenu, nayaandikia haya kwamba: Nitakapokuwako kwenu nisitumie ukali wa kukata maneno; nguvu ya kuvifanya hivyo nimepewa na Bwana, lakini ni ya kujenga, siyo ya kujengua. Mwisho, ndugu, furahini, mtengenezane, mwonyane, mioyo yenu iwe mmoja, mpate kutengemana! Ndipo, Mungu aliye mwenye upendo na matengemano atakapokuwa pamoja nanyi. Mwamkiane mkinoneana, kama watakatifu walivyozoea! Watakatifu wote wanawasalimu. Upole wa Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu na bia ya Roho Mtakatifu iwakalie ninyi nyote! Amin. Mimi Paulo ni mtume, lakini sikutumwa na watu wala kwa agizo la mtu, ila nimetumwa kwa agizo lake Yesu Kristo nalo lake Mungu Baba aliyemfufua katika wafu. Mimi pamoja na ndugu wote walio pamoja nami tunawaandikia ninyi wateule wa Galatia. Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo! Ndiye aliyejitoa kwa ajili ya makosa yetu, apate kutuokoa katika dunia hii mbaya ya sasa. Ndivyo, Mungu, Baba yetu, alivyotaka. Huyu atukuzwe kale na kale pasipo mwisho! Amin. Nastaajabu, ya kuwa mwageuzwa upesi hivyo, mwondoke kwake yeye aliyewaita, mgawiwe kipaji chake Kristo, mkafuata utume mwema mwingine. Tena hakuna utume mwema mwingine, ila wako watu tu wanaowahangaisha; ndio wanaotaka kuugeuza Utume mwema wa Kristo. Lakini ikiwa sisi, au ijapo malaika wa mbinguni, akiwatangazia utume mwema mwingine kuliko ule, tuliowapigia sisi, na awe ameapizwa! Tuliyoyasema sasa hivi, narudia kuyasema tena: Mtu akiwatangazia utume mwema mwingine kuliko ule, mlioupokea, na awe ameapizwa! Je? Hayo nayasemea kuitikiwa nao watu au naye Mungu? Au je? Natafuta kuwapendeza watu? Kama ningependeza watu bado, basi, singekuwa mtumwa wake Kristo. Ndugu zangu, nawatambulisha, ya kuwa Utume mwema uliotangazwa nami sio wa kimtu. Kwani nami sikuupokea kwa mtu, wala sikufundishwa, ila nimefunuliwa na Yesu Kristo. Kwani mmesikia, nilivyoendelea hapo, nilipolifuata tambiko la Kiyuda, ya kuwa nalijipingia kuwafukuza wateule wa Mungu na kuwajengua. Nami hapo, nilipolifuata tambiko la Kiyuda, nikapita wenzangu wengi, ambao tulizaliwa nao mwaka mmoja, maana nilikaza kujihimiza, niandamane nayo, tuliyoyapokea kwa baba zetu. Lakini Mungu alikuwa amenitenga hapo, nilipokuwa tumboni mwa mama yangu, akaniita, nigawiwe kipaji chake. Hapo, alipopendezwa kumfunua Mwana wake moyoni mwangu, kusudi nije, niwapigie wamizimu hiyo mbiu yake njema, papo hapo nikakata mawazo pasipo kuuliza mwili wangu ulio wenye nyama na damu, wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwao waliokuwa mitume mbele yangu, ila nalikwenda Arabuni, kisha nikarudi tena Damasko. Miaka mitatu ilipokwisha kupita, nikapanda kwenda Yerusalemu, nijuane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini hakuna mtume mwingine, niliyemwona, asipokuwa Yakobo, nduguye Bwana. Lakini haya, ninayowaandikia, tazameni, Mungu anayajua, ya kuwa sisemi uwongo. Kisha nikafika upande wa Ushami na Kilikia. Nami nilikuwa sijajulikana uso kwa uso nao wateule wake Kristo walioko Yudea. Ila walikuwa wamesikia tu: Yule aliyetufukuza kwanza sasa huipiga hiyo mbiu njema ya kumtegemea Bwana, alikokuwa amekujengua. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu. Kisha miaka kumi na minne ilipopita, nikapanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua naye Tito, aende pamoja nami. Lakini nalipanda kwa kutumwa na ufunuo, nilioupata. Nikawaelezea Utume mwema, ninaowapigia wamizimu. Kupita wengine naliwaelezea wale waliowaziwa kuwa wenye cheo, wavione hivyo, ninavyovikimbilia sasa, navyo nilivyovikimbilia mbele, kama ni vya bure. Lakini hata Tito aliyekuwa pamoja nami hakushurutishwa kutahiriwa, angawa ni Mgriki. Lakini kulikuwako ndugu wa uwongo waliokuwa wamejiingiza na kufichaficha; hao waliingia tu, watupeleleze, tunavyomkalia Yesu Kristo pasipo mwiko wo wote, waturudishe katika utumwa wa miiko. Nasi hatukushindika, tuwatii hao, hata saa moja tu, kwamba huo Utume mwema ufulize kujulikana kuwa wa kweli. Lakini waliowaziwa kuwa wenye cheo hivyo, walivyo kale, si kitu kwangu, maana Mungu hatazami uso wa mtu. Nasema: Nao hao walioambiwa kuwa wenye cheo hawakuniongezea jambo; lakini wakaona kweli, ya kuwa mimi nimepewa kuutangaza Utume mwema kwao wasiotahiriwa, kama Petero alivyopewa kuutangaza kwao waliotahiriwa. Kwani aliyempa Petero nguvu ya kuwa mtume wao waliotahiriwa ndiye aliyenipa nami nguvu ya kuwa mtume wao wamizimu. Walipokitambua kipaji, nilichogawiwa, ndipo, Yakobo na Kefa na Yohana wanaowaziwa kuwa nguzo walipotupa mimi na Barnaba mikono kwamba: Tu mmoja, sisi tuipige hiyo mbiu kwao wamizimu, lakini wao kwao waliotahiriwa. Walitutakia hilo moja tu, tuwakumbuke maskini wao; nami nimejipingia kulitimiza hili. Lakini Kefa alipofika Antiokia, nikambishia usoni pake, kwani alichongewa. Maana kulikuwako waliotumwa na Yakobo; hao walipokuwa hawajaja bado, alikula pamoja na wamizimu. Lakini walipokuja, akatoweka na kujitenga, kwani aliwaogopa wale waliotahiriwa. Nao wenzake wa Kiyuda waliokuwako wakaufuata huo ujanja wake, naye Barnaba akaponzwa na huo ujanja wao. Lakini nilipowaona, ya kuwa hawaishiki njia nyofu wakiifuata kweli ya Utume mwema, nikamwambia Kefa mbele yao wote: Wewe u Myuda; tena mwenendo wako ni wa kimizimu, sio wa Kiyuda; imekuwaje, wewe ukiwashurutisha wamizimu kufanya mwenendo wa Kiyuda? Sisi tumezaliwa kuwa Wayuda, hatu wakosaji waliotoka kwao wamizimu. Lakini twajua: mtu hapati wongofu akiyafanya Maonyo, ila hupata wongofu akimtegemea Kristo Yesu; nasi tukamtegemea Kristo Yesu, tupate wongofu kwa kumtegemea Kristo, siko kwa kuyafanya Maonyo. Kwani hakuna aliye wa kimtu atakayepata wongofu kwa kuyafanya Maonyo. Lakini sisi tunaotaka kupata wongofu kwa kuwa wake Kristo, sasa wenyewe tukionekana kuwa wakosaji, je? Kristo naye siye mwenye kutumikia makosa? La, sivyo! Kwani nikiyajenga tena yale, niliyoyajengua, naonyesha, ya kama sipatani na mimi mwenyewe. Kwani hapo, niliposhindwa na Maonyo, ndipo, nilipoyafika Maonyo, nipate kumkalia Mungu, maana nimewambwa msalabani pamoja na Kristo. Tena ninaishi, lakini sasa si mimi tena ninayeishi, ila Kristo ndiye anayeishi mwilini mwangu. Maana hivyo, ninavyoishi sasa mwilini, ninaishi kwa kumtegemea Mwana wake Mungu aliyenipenda, akajitoa kwa ajili yangu. Gawio la Mungu silitangui. Kwani kama wongofu ungepatikana kwa kuyafanya Maonyo, basi, Kristo angekuwa amekufa bure. Enyi Wagalatia, hamna akili? Ni uganga gani uliowashinda, msiyatii yaliyo ya kweli? Mmeonyeshwa Yesu Kristo, mmtazame kwa mambo yenu, alivyowambwa msalabani. Neno hili tu nataka kuambiwa nanyi: Mmempokea Roho kwa kuyafanya Maonyo au kwa kuyategemea, mliyoyasikia? Imekuwaje, akili zikiwapotea hivyo? Mliyoyaanza Rohoni, mwataka kuyamaliza sasa miilini? Yale yote mmeteswa bure? Kweli siyo ya bure! Ilikuwaje? Aliyewapa Roho na kufanya yenye nguvu kwenu aliyafanyia kwamba: Mmeyafanya Maonyo? au kwamba: Mmeyategemea, mliyoyasikia? Ndivyo, yalivyokuwa nayo ya Aburahamu: Akamtegemea Mungu, kwa hiyo akawaziwa kuwa mwenye wongofu. Kwa hiyo yatambueni: wenye kumtegemea Mungu hao ndio wana wa Aburahamu! Lakini Maandiko yaliona kale, ya kuwa Mungu huwapatia wamizimu wongofu, wakiwa wanamtegemea. Kwa hiyo alimpigia Aburahamu kale mbiu ile njema: Mwako ndimo, mataifa yote yatakamobarikiwa. Kwa hiyo wenye kumtegemea Mungu hubarikiwa pamoja na Aburahamu aliyekuwa mtegemevu. Kwani wote walio wenye kuyafanya Maonyo hawajatoka bado kwenye kuapizwa. Kwani imeandikwa: Na awe ameapizwa kila mtu asiyeandamana nayo yote yaliyoandikwa katika chuo cha Maonyo, ayafanye! Lakini neno hili ni waziwazi, ya kuwa hakuna mtu atakayepata wongofu kwake Mungu, kwa kuyafanya Maonyo, kwani: Mwongofu atapata uzima kwa kumtegemea Mungu. Lakini Maonyo hayakutoka kwenye kumtegemea Mungu, ila: Atakayeyafanya atapata uzima kwa njia hiyo. Kristo alitukomboa, tusiapizwe na Maonyo, alipoapizwa kwa ajili yetu, kwani imeandikwa: Kila aliyetundikwa mtini ameapizwa. Hivyo mbaraka yake Aburahamu imewafikia wamizimu hapo, Yesu Kristo alipotokea, nasi tukipokee kiagio cha Roho tukiwa twamtegemea. Ndugu, niseme kimtu: Agano la mtu aliyekufa hakuna alitanguaye, likiisha kusimikwa, wala aliongezaye neno. Lakini Aburahamu alikuwa amepewa viagio vile yeye nao uzao wake. Hasemi: Wazao, kama ni wengi, ila kama ni mmoja, asema: Nao uzao wako, nao huo ndiye Kristo. Kwa hiyo nasema: Agano limetangulia kusimikwa na Mungu, Maonyo yakatokea nyuma, miaka 430 ilipopita; hayawezi kulitangua agano, wala hayawezi kukikomesha nacho kiagio. Kwani huo urithi kama ungalipatikana kwa kuyafanya Maonyo usingepatikana tena kwa kupewa kiagio. Lakini Mungu alimgawia Aburahamu huohuo alipompa kiagio. Basi, Maonyo yako na maana gani? Yalitolewa siku za kati kwa ajili ya mapitano, mpaka atakapokuja yule mzao aliye mwenye kiagio. Nayo Maonyo hapo, yalipotolewa, yalitumikiwa na malaika, yakawekwa mkononi mwa mpatanishaji. Lakini mpatanishaji siye wa mmoja tu, lakini Mungu ni mmoja. Tena je? Maonyo huvikataa viagio vya Mungu? La, sivyo! Kwani kama yangekuwako Maonyo yaliyotolewa kuwa yenye nguvu ya kuwapa watu uzima, wongofu ungepatikana kweli kwa kuyafanya maonyo. Lakini Maandiko yamewafunga wote pamoja kuwa watumwa wa makosa kwamba: Wote watakaomtegemea wapewe kile kiagio kitokacho kwenye kumtegemea Yesu Kristo. *Lakini tegemeo lilipokuwa halijatokea bado, tulilindwa, tuyatii Maonyo, tukawa tumefungwa pamoja, tungoje, tegemeo litakapofunuliwa. Hivyo ndivyo, Maonyo yalivyotuongoza kama watoto, yakatupeleka kwake Kristo, tupate wongofu kwa kumtegemea. Lakini tangu hapo, tegemeo lilipotokea, hatushikwi tena na mwongozi. Kwani ninyi nyote m wana wa Mungu kwa kumtegemea mkiwa wake Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatiziwa Kristo mmemvaa Kristo. Kwake yeye hakuna tena Myuda na Mgriki, wala mtumwa na mwungwana, wala mume na mke, kwani ninyi nyote m mmoja kwa kuwa wake Kristo Yesu. Nanyi mkiwa wake Kristo, basi, mmekuwa hata uzao wake Aburahamu, tena m warithi kwa kiagio, mlichowekewa.* Nasema: Kibwana siku anapokuwa mchanga bado, hakuna, apitanacho na mtumwa, angawa ni bwana wa vyote, ila hana budi kuwatii walezi na watunza mali, mpaka siku zitimie zilizowekwa na baba yake. Vivyo hivyo nasi tulipokuwa wachanga tulikuwa tumeyatumikia kitumwa mambo ya kwanza ya humu ulimwenguni. Lakini siku zilipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe, akizaliwa na mwanamke, akawa akiyatii Maonyo, kusudi awakomboe walioyatii Maonyo, kwamba tupate kuwa wana. Kwa sababu m wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe, aingie mioyoni mwetu, ndiye anayetuombea na kulia: Ee, Baba yetu! Kwa hiyo hu mtumwa tena, ila umekuwa mwana. Lakini kama umekuwa mwana, umekuwa hata mrithi wa Mungu kwa kuwa wake Kristo.* Lakini hapo kale, mlipokuwa hammjui Mungu, mlitumikia miungu isiyo miungu kwa hivyo, ilivyo. Lakini sasa, mnapomtambua Mungu, tena mnapotambulikana kwake Mungu, mwaigeukiaje tena ile miiko ya kale ikosayo nguvu, iletayo ukiwa tu? Mwatakaje, mwanze kuitumikia tena? Mwaangalia sana siku na miezi na miongo na miaka. Naogopa kwa ajili yenu kwamba: Labda nimejisumbua kwenu bure. Ndugu, nawabembeleza, mwe, kama mimi nilivyo! Maana, mimi ni kama ninyi. Hamkunipotoa lo lote. Lakini mwajua: hapo kwanza nilipowapitia hiyo mbiu njema nilikuwa mnyonge wa mwili; nikawapo nikijaribiwa na mambo yale ya mwili wangu, lakini hamkunibeua, wala hamkunifukuza, ila mmenipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu mwenyewe. Yale mashangilio yenu sasa yako wapi? Kwani nawashuhudia ninyi kwamba: Kama ingaliwezekana, mngaliyang'oa hata macho yenu, mkanipa. Je? Nimegeuka kuwa mchukivu wenu kwa kuwaambia yaliyo ya kweli? Wanavyowahimiza, si vizuri, ila wanataka kuwatenganisha na sisi, mpate kujihimiza kuwatumikia wao. Ni vizuri kujihimiza kwa ajili ya jambo zuri po pote, msijihimize hapo tu, nikiwako kwenu. Watoto wangu, ninao uchungu, kama nitawazaa mara ya pili, mpaka Kristo aonekane kuwa yumo mwenu. Ingefaa, niwe kwenu sasa, nikaweza kuigeuza sauti yangu, maana ninawahangaikia ninyi. Mniambie ninyi mnaotaka kujitwika Maonyo: Hamyasikii Maonyo? Kwani imeandikwa: Aburahamu alikuwa na wana wawili waume, mmoja wa kijakazi, mmoja wa mkewe mwenyewe. Lakini yule wa Kijakazi alizaliwa kwa tamaa ya mwili, lakini yule wa mwungwana alizaliwa kwa nguvu ya kiagio Mambo hayo yako na maana: kwani wale wanawake wawili ndio maagano mawili. La kwanza ndilo lililotokea mlimani kwa Sinai, linalozaa watumwa tu; hili ndio Hagari. Maana mlima wa Sinai huitwa Hagari kule Arabuni; nao umelingana na Yerusalemu wa sasa, kwani uko utumwani pamoja na watoto wake. Lakini ule Yerusalemu wa juu ndio yule mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi. Kwani imeandikwa: Shangilia, wewe uliye mgumba, usiyezaa! Jichekelee na kupaza sauti, wewe usiyeona uchungu wa kuzaa! Kwani wana wake yule aliye peke yake ni wengi kuliko wana wake yule aliye na mumewe. Lakini ninyi ndugu, mmekuwa wana wa kiagio kama Isaka. Lakini kama hapo kale yule aliyezaliwa kwa tamaa ya mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa nguvu ya Roho, ndivyo, vilivyo hata sasa. Lakini Maandiko yasemaje? Mfukuze huyu kijakazi pamoja na mwanawe! Kwani mwana wa kijakazi hatapata urithi pamoja na mwana wa mwungwana. Kwa hiyo, ndugu, sisi hatu watoto wa kijakazi, ila wake mwungwana. *Kristo ametukomboa, tuwe waungwana. Kwa hiyo simameni, msijitie tena katika mafungo ya utumwa! Tazameni, mimi Paulo nawaambiani: Kristo hatawafaa kitu, mkitahiriwa. Tena namshuhudia kila mtu aliyetahiriwa, ya kuwa ni mdeni wa kuyafanya Maonyo yote. Ninyi mtakao kupata wongofu kwa kuyafanya Maonyo mmetengwa na Kristo, mmeanguka na kuyaacha magawio. Kwani sisi kwa nguvu ya Roho twakishika kingojeo cha kwamba: Tutapata wongofu kwa kumtegemea Mungu. Maana tukiwa naye Kristo Yesu, kunakotupa nguvu siko kutahiriwa, wala kutotahiriwa, ila kumtegemea Mungu kutimilikako katika kupendana. Mlianza kushika njia nzuri; yuko nani aliyewakwaza, msiyatii yaliyo ya kweli? Kazi hii ya kuwavutavuta hivyo haikutoka kwake yeye aliyewaita. Chachu kidogo hulichachusha donge lote. Hivyo, mlivyo naye Bwana, mimi huwawazia kuwa welekevu kwamba: Hamtaigeuza mioyo. Lakini aliyewahangaisha hivyo ataiona hukumu yake, awaye yote. Lakini mimi, ndugu, kama ningetangaza hata sasa, watu watahiriwe, ningekuwa mwenye kufukuzwa? Nayo makwazo ya msalaba yangekuwa yameondolewa. Ingefaa, wale wenye kuwatukusa wakatwe na kutengwa. Ndugu, ninyi mliitiwa kuwa waungwana. Lakini uungwana huo msiugeuze kuwa tokeo la tamaa za miili yenu, ila mtumikiane na kupendana! Kwani Maonyo yote hutimilika katika neno moja, ndilo hili: Umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwenyewe! Lakini mkiumana, mkilana ninyi kwa ninyi, angalieni, msimezwe kabisa kwa kule kulana.* *Lakini nasema, mwendelee Kiroho! Hivyo hamtaweza kuzitimiza tamaa za miili. Kwani miili huyatamani yanayokataliwa na Roho, naye Roho huyatamani yanayokataliwa na miili; hawa wawili hupingana, msipate kuyafanya, myatakayo. Lakini mkiongozwa na Roho ham tena watumwa wa Maonyo. Nayo matendo ya miili yako waziwazi, ndiyo ugoni, uchafu, uasherati, kutambikia vinyago, uchawi, uchukivu, ugomvi, wivu, mifundo ya mioyo, machokozi, matengano, vyama, kijicho, ulevi, ulafi, nayo mambo mengine yaliyofanana nayo. Kama nilivyowaambia kale, vivyo hivyo nawaambia tena: Wafanyizao mambo kama hayo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini mazao ya Roho ndiyo haya: upendano, furaha, utengemano, uvumilivu, utu, wema, welekevu, utulivu, kuzishinda tamaa. Mambo kama hayo hayakataliwi na Maonyo. Lakini wa Kristo Yesu huiua miili na kuiwamba msalabani pamoja na mawazo mabaya na tamaa.* *Tukiwa wa Kiroho na tuendelee Kiroho! Tusitafute utukufu ulio wa bure, tukichokozana, tena tukioneana kijicho! Ndugu, mtu akipatikana ameanguka, ninyi mlio wa Kiroho, mwonyeni Kiroho kwa upole, ashupae tena! Jiangalie mwenyewe, usijaribiwe nawe! Mchukuliane mizigo! Hivyo mtayatimiza Maonyo yake Kristo. Kwani mtu akijiwazia kuwa mwenye nguvu, tena siye, hujidanganya mwenyewe. Lakini kila mtu azitazame kazi zake mwenyewe, ziwe nzuri! Ndipo, atakapojivuma moyoni tu, asitolee wengine majivuno yake. Kwani kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe. Lakini mwenye kufundishwa lile Neno na amgawie mfunzi mema yote, aliyo nayo! Msidanganyike, Mungu habezwi! Kwani mtu aliyoyapanda, ndiyo, atakayoyavuna. Maana mwenye kupanda mwilini mwake atavuna humo mwilini kuoza. Lakini mwenye kupanda Rohoni atavuna humo Rohoni uzima wa kale na kale. Tusichoke kuyafanya yaliyo mazuri, kwani siku zake zitakapotimia, tutavuna pasipo kukoma. Basi, kwa sababu tuko nchini bado, wote na tuwatendee mema, lakini kuliko wengine wenzetu wa kumtegemea Bwana!* Yatazameni haya maandiko yote, niliyowaandikia kwa mkono wangu mimi! Wote wanaotaka kupendeleza miili, hao huwashurutisha kutahiriwa; tena hapana neno jingine, ni kwamba tu: Wasifukuzwe kwa ajili ya msalaba wake Kristo. Kwani nao wenyewe waliotahiriwa hawayashiki Maonyo, ila hutaka, ninyi mtahiriwe, wapate kujivunia miili yenu. Lakini mimi sitaki kujivuna, isipokuwa kwa ajili ya msalaba wake Bwana wetu Kristo, maana mlemle mimi nimefiwa na ulimwengu, nao ulimwengu umefiwa na mimi mlemle. Kwani ukiwa naye Kristo Yesu, kutahiriwa siko, wala kutotahiriwa siko, ila kuwa kiumbe kipya ndiko. Nao wote wanaoendelea na kujipingia hivyo na watengemane, upole uwakalie pamoja nao Waisiraeli wa Mungu! Basi, tangu sasa asionekane atakayenisumbua tena! Kwani mwilini mwangu mimi ninayo makovu ya Yesu. Upole wa Bwana wetu Yesu Kristo uzikalie roho zenu, ndugu! Amin. Mimi Paulo niliye mtume wa Kristo Yesu kwa hayo, Mungu ayatakayo, nawaandikia ninyi watakatifu mlioko Efeso, nanyi mliomtegemea Kristo Yesu: Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo! *Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetugawia mema yote ya kiroho yatokayo mbinguni kwake Kristo! Kwani ulimwengu ulipokuwa haujaumbwa bado, alituchagua sisi kuwa wake yeye, tuwe watakatifu machoni pake pasipo kilema. Kwa hivyo, anavyotupenda, alitutenga kale, tupokelewe kuwa wana wake mwenyewe tukimfuata Yesu Kristo; ndiyo yaliyompendeza, akayataka, yawepo. Nasi huusifu utukufu wa kipaji chake, alichotugawia hapo, alipomtoa mpendwa wake. Katika damu yake yeye ndimo, tupatiamo ukombozi, maana twaondolewa makosa; hayo ndiyo magawio yake mengi yaliyotuongezea nasi werevu wote ulio wa kweli, hata ujuzi wote. Kisha akatutambulisha, ayatakayo, yaliyokuwa yamefichwa. Ndivyo, ylivyompendeza, akayaweka kale moyoni mwake, yatengenezeke, siku alizoziweka zitakapotimia, Kristo awe kichwa chao yote yaliyoko mbinguni nacho chao yaliyoko nchini. Yeye ndiye, ambaye tulipatiwa naye urithi wetu, tuliokatiwa kale na kuwekewa kale, maana yeye huyafanya yote, yawepo, kama ayatakavyo mwenyewe. Kwa hiyo sisi tuliotangulia kumngojea Kristo ndio tutakaousifu utukufu wake. Nanyi mmelisikia Neno la kweli, ni ule Utume mwema wa wokovu wenu; napo hapo, mlipolitegemea, mlitiwa muhuri yake mlipompata Roho Mtakatifu, tuliyeagiwa. Huyu ni rehani ya urithi wetu, tujue: tumekombolewa, tu watu wake, utukufu wake upate wenye kuusifu.* *Kwa hiyo mimi niliposikia, mnavyomtegemea Bwana Yesu, tena mnavyowapenda watakatifu wote, sichoki kushukuru kwa ajili yenu kila, niwakumbukapo nikiomba. Nawaombea, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye utukufu, awape roho ya werevu wa kweli na ya ufunuzi, mmtambue yeye alivyo. Namo mioyoni mwenu atiemo macho yaliyoangazwa, mpate kujua, kilivyo hicho kingojeo, mlichoitiwa naye, tena mwujue nao utukufu wa urithi wake, aliowawekea watakatifu, ulivyo mwingi. Mpate kuujua nao uwezo wake, unavyokua kuupita wote mwingine ulioko; huo akatupa sisi tumtegemeao kwa kuhimizwa na nguvu zake kuu. Ndizo, alizozitumia alipomfufua Kristo katika wafu na kumketisha kuumeni kwake mbinguni na kumpa cheo kuupita ukubwa na ufalme na uwezo na ubwana wote na kuyapita majina yo yote yatakayotajwa siku hizi, nazo siku zote zitakazokuja. Akayaweka yote kuwa chini migguni pake, naye mwenyewe akamfanya kuwa mkuu peke yake, awe kichwa chao wateule wote, maana wao ni mwili wake; huu ndio utimilifu wake yeye anayeyatimiza yote pia kwao wote po pote pasipo kusaza.* Nanyi mlikuwa mmekufa kwa ajili ya maanguko na makosa yenu, mliyoendelea nayo kale kwa desturi za watu walio wa ulimwengu huu tu; ndivyo, mwenye kuzitawala nguvu za angani atakavyo, ni yule pepo anayetenda nguvu hata sasa mwao waliokataa kutii. Nasi sote kale tulikuwa wenzao tulipoendelea na kuzifuata tamaa za miili yetu na kuyafanya, miili na mioyo yetu iliyoyataka, nasi kwa hivyo, tulivyokuwa hapo, tulikuwa wana waliomkasirisha kama wale wengine. *Lakini Mungu alikuwa ametulimbikia huruma kwa kuwa na upendo mwingi wa kutupenda; kwa sababu hiyo akaturudisha uzimani pamoja na Kristo hapo, tulipokuwa tumekufa kwa ajili ya maanguko; hivyo wokovu wenu ni gawio tu. Alipokwisha kutufufua pamoja naye akatukalisha mbinguni pake Kristo Yesu. Maana siku zitakazokuja anataka kuonyesha, magawio yake yanavyokuwa mengi, yasipimike akituendea kwa utu tu katika Kristo Yesu. Kwani wokovu wenu ni gawio tu, mlilopewa kwa ajili ya kumtegemea, nako hakukutoka mwenu, maana nako ni kipaji chake Mungu, nacho hamkukipata kwa kazi zenu, mtu asipate kujivuna. Kwani sisi tu kazi yake yeye, namo mwake Kristo Yesu ndimo, tulimoumbiwa, tufanye matendo mema, Mungu aliyotutengenezea kale, tuyafuate.* Kwa hiyo yakumbukeni: kale mlikuwa wamizimu kwa hivyo, miili yenu ilivyo; mkaitwa mapumbavu nao wale waliojiita makungwi, kwa sababu walikuwa wametahiriwa na mikono ya watu miilini mwao. Kumbukeni: siku zile mlikuwa hamnaye Kristo, tena mlikuwa mmekatazwa kuwa wenyeji kwao Waisiraeli, mkawa wageni, msiyajue maagano, waliyoagiwa kuyapata. Mlikuwa hamnacho kingojeo, wala hamnaye Mungu huku ulimwenguni. Lakini sasa kwa kuwa wake Kristo Yesu nanyi mliokuwa kale mbali mmeletwa na damu ya Kristo, mfike karibu. Kwani yeye ni utengemano wetu, maana yale makundi mawili aliyageuza kuwa moja, akiuvunja ukingo uliotutenga, tuchukizane. Ilikuwa hapo, alipoyatangua mwilini mwake yale maonyo na maagizo yaliyokuwa ya miiko tu. Akataka kuwaumba hao wote wawili kuwa mtu mmoja mpya aliye wake yeye; kwa hiyo aliwapatanisha, akawa kole yao wote wawili alipomlipa Mungu madeni yao yeye mmoja mwilini mwake, alipowambwa msalabani; huko ndiko, alikoyaua yale machukivu. Kisha akaja kuipiga hiyo mbiu njema ya utengemano kwenu ninyi mliokuwa mbali, nako kwao waliokuwa karibu. Kwani kwake yeye sote wawili tumepata njia ya kumfikia Baba, tukiwa wenye Roho moja. *Kwa hiyo sasa ham wageni tena, wala wenye kukaa kando, ila m wenyeji pamoja nao watakatifu, tena m wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wao mitume na wafumbuaji, ambao Kristo Yesu ni jiwe lake la pembeni. Kwa nguvu yake yeye jengo lote linaunganishwa, lipate kukua, mpaka liwe nyumba takatifu, Bwana alimo. Humu nanyi mnajengwa pamoja na wengine, mwe kao lake Mungu la Kiroho.* Hayo yamenipeleka mimi Paulo kifungoni kuwa mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi wamizimu. Labda mmesikia, Mungu alivyonipa utunzaji wa magawio yake, niwagawie nanyi. Nilifumbuliwa, niyatambue yale yaliyofichwa tangu kale, kama nilivyowaandikia kidogo hapo kwanza. Mkiyasoma mwaweza kuuona ujuzi wangu wa fumbo la Kristo. Siku zilizopita zote wana wa watu hawajatambulishwa fumbo hilo, ambalo mitume na wafumbuaji wake watakatifu walifunuliwa sasa na Roho, hilo la kwamba: Wamizimu nao ndio wenye urithi pamoja nasi, kwamba: Nao wamo pamoja nasi mwilini mwake, kwamba: Nao ni wenye kiagio, tulichopewa katika Kristo Yesu tulipotangaziwa Utume mwema. Ndio, niutumikiao nami kwa hivyo, Mungu alivyonigawia kipaji changu, nilichopewa hapo, niliposhindwa na nguvu zake. Mimi niliye mdogo kuliko watakatifu wote nikapewa gawio hili, niwapigie wamizimu mbiu njema ya mema yote ya Kristo yaliyo mengi, yasiwezekane kupelelezeka yote; kisha niueleze vema utunzaji wa lile fumbo lililokuwa limefichwa tangu zamani zote kwake Mungu aliyeviumba vyote. Maana siku hizi sharti wakubwa na wanguvu wote walioko mbinguni watambulishwe na wateule, ujuzi wake Mungu ulivyo mwingi sana. Mwenyewe aliviweka hivyo kale kabisa moyoni mwake, vitimie katika Kristo Yesu, Bwana wetu; kisha akatuongoza njia ya kumwendea pasipo woga wowote, mpaka tumfikie tukiwa tumejishikizia kwake yeye kwa kumtegemea. Kwa hiyo naomba, msichoke kwa ajili ya maumivu yangu, niliyopatwa nayo kwa ajili yenu, maana yanawapatia utukufu. Kwa sababu hii nampigia Baba na Bwana wetu Yesu Kristo magoti; kwani kila aliye baba, kama yuko mbinguni au yuko nchini, hujiita na jina hili la baba. Nawaombea, kwa wingi wa utukufu wake awape, mtu wenu wa ndani apate nguvu akikuzwa na Roho wake. Tena awape, Kristo akae mioyoni mwenu kwa hivyo, mnavyomtegemea, mpate kushusha mizizi katika upendo, mshikizwe nayo! Kisha awape, mweze kupima pamoja na watakatifu wote, upendo ulivyo mpana na mrefu, tena unavyoingia chini, hata unavyokwenda juu; ndivyo, mtakavyoutambua upendo wake Kristo, ya kuwa unaupita utambuzi wote, mpate kuujaa katika mambo yote, kama Mungu alivyoujaa. Lakini yeye kwa hivyo, nguvu yake inavyokaza mwetu, anaweza kufanya kuyapita yote, tuyaombayo nayo tuyawazayo, yeye atukuzwe kwao wateule walio wake Kristo Yesu siku zote zitakazokuwapo kale na kale pasipo mwisho! Amin.* *Mimi niliyefungwa kwa ajili ya Bwana nawaonya ninyi, mfanye mwenendo unaopatana na wito, mlioitiwa. Mwe wenye unyenyekevu wote na upole na uvumilivu, mvumiliane mkipendana! Kwa hivyo, Roho alivyowageuza kuwa mmoja, mjikaze kujiunga kwa mapatano! Mwili ni mmoja, nayo Roho ni moja, nacho kingojeo cha wito wenu, mlichoitiwa, ni kimoja. Bwana ni mmoja, nalo tegemeo ni moja, nao ubatizo ni mmoja, naye Mungu ni mmoja, ndiye Baba yao wote, ni mwenye kuwatawala wote, ni mwenye kuwaendesha wote, ni mwenye kuwakalia wote.* Lakini sote tumegawiwa kipaji, kila mmoja chake yeye, kama Kristo alivyompimia cha kumpa. Kwa hiyo yamesemwa: Alipopaa juu aliteka mateka, akawapa watu vipaji. Basi, neno hili: “alipaa” ni kwambaje isipokuwa kwamba: Alishuka kwanza kwenda pande za kuzimuni kwa nchi? Aliyeshuka ndiye yule yule aliyepaa kuzipita mbingu zote, apate kuyatimiza yote. *Naye akawapa wengine kuwa mitume, wengine wafumbuaji, wengine wapiga mbiu njema, wengine wachungaji na wafunzi, maana watakatifu watengenezwe, wajue kuzifanya kazi za utumishi; ndizo kazi za kuujenga mwili wake Kristo, mpaka sisi sote tutakapofikia kuwa mmoja wa kumtegemea na wa kumtambua Mwana wa Mungu; huko ndiko kukua kwenyewe na kuutimiza umri unaoweza kuutambua wingi wote wa vipaji vya Kristo. Hivyo hatutakuwa tena wachanga wanaochukuliwa kama mawimbi na kupelekwa huko na huko na mafunzo ya watu yanayogeukageuka kama upepo, maana ni ya uwongo na ya udanganyi wa watu wanaotaka kutupoteza kwa werevu mbaya. Ila tutakuwa wenye kupendana kweli, katika mambo yote tumkalie yeye Kristo aliye kichwa chetu. Naye ndiye mwenye kuunganisha mwili wote, ukishikamizwa na mafundo yote yanayoutia nguvu, kila fundo moja, kama lilivyopimiwa kazi yake; hivyo mwili hukua, ukijengwa kuwa mzuri kwa kupendana.* Neno hili sasa nalisema na kumtaja Bwana, awe shahidi wangu: Msiendelee tena, kama wamizimu nao wanavyoendelea na kufuata mambo wasiyoyajua maana! Mawazo yao yameguiwa na giza, uzima wa Mungu ukawa kitu kigeni kwao kwa ajili ya ujinga, walio nao, na kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Hivyo, walivyokufa ganzi la mioyo, wakajitia katika uasherati, wakayafanya machafu yote wakijipatiamo mali. Lakini ninyi hamkufundishwa mambo ya Kristo kuwa hivyo. Kwani mmesikia, mkafundishwa Neno lake kwamba: Iliyo ya kweli imo mwake Yesu. *Kwa hivyo, mlivyoendelea kale, mvueni mtu wa kale aliyejiponza kwa kuzifuata tamaa za udanganyifu! Kisha mawazo ya mioyo yenu yarudishiwe upya wa Kiroho, mmvae mtu mpya aliyeumbwa kuwa wa Kimungu mwenye wongofu na utakatifu wa kweli! Kwa hiyo uvueni uwongo, mwambiane yaliyo ya kweli kila mtu na mwenzake! Kwani tu viungo, kila mmoja kiungo cha mwenzake. Mioyo inapojaa makali, msikose! Jua lisiwachwee, mkingali na makali yenu, wala msimpe Msengenyaji mahali pa kukaa mwenu! Aliyekwiba asiibe tena! Ila sharti ajisumbue na kufanya kazi kwa mikono yake mwenyewe, ajipatie mema, naye aone ya kumgawia mwenye kuyakosa! Maneno yo yote yaliyo maovu yasitoke vinywani mwenu! Ila kama liko neno zuri lifaalo la kujenga palipojenguka lisemeni, liwapendeze wenye kulisikia! Msimsikitishe Roho Mtakatifu wa Mungu! Kwani ndiye, mliyepewa kuwa muhuri yenu ya siku ya ukombozi. Uchungu wo wote na mifundo ya mioyo na makali na mateto na matusi na yaondoke kwenu pamoja na uovu wote! Mwendeane kwa utu na kwa upole, mkiacha kulipishana, kama Mungu naye alivyoacha kuwalipisha ninyi kwa kuwa wake Kristo!* Mwigeni Mungu, kama inavyowapasa watoto wapendwa! Tena mwendeane na kupendana, kama Kristo alivyowapenda ninyi! Akajitoa kwa ajili yetu sisi kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuuawa, Mungu asikie mnuko mzuri. Lakini mambo ya ugoni na ya uchafu wo wote na ya choyo yasitajwe kwenu kamwe, kama inavyowapasa watakatifu; wala matusi wala mapuzi wala mafyozi mabaya, maana siyo yafaayo; yafaayo ni ya kushukuru. Kwani haya yajueni na kuyatambua vema: hakuna mgoni wala mchafu wala mwenye choyo aliye mtambikia vinyago atakayepata fungu katika ufalme wa Kristo na wa Mungu. Pasioneke mwenye kuwadanganya na maneno yasiyo na maana! Kwani kwa ajili yao makali ya Mungu huwajia wakataao kutii. Kwa hiyo msichanganyike nao! Kwani kale mlikuwa giza, lakini sasa mmekuwa mwanga kwa kuwa naye Bwana. Mwendelee, kama iwapasavyo wana wa mwanga! Kwani matunda yanayozaliwa mwangani ndio wema wo wote na wongofu na ukweli.* Pambanueni, kama ni mambo gani yampendezayo Bwana! Msiwe wenzao wenye kuzifanya kazi za giza zisizofaa, ila mkaze kuwaumbua! Kwani hutia soni kuyataja tu yanayofanywa nao na kuyafichaficha. Lakini yote hufunuliwa yakiumbuliwa na mwanga, kwani kila kitu kinachofunuliwa huangazika. Kwa hiyo husema: Amka, wewe uliyelala! Inuka, utoke kwenye wafu! Kisha Kristo atakuangaza. *Kwa hiyo angalieni sana, mtakavyoendelea! Msiwe wenye ujinga, ila mwe wenye werevu wa kweli! Mzitumie vema siku za sasa! Kwani siku hizi ndizo mbaya. Kwa hiyo msipumbae, ila mjijulishe, Bwana ayatakayo! Wala msilewe pombe! Kwani hazikomeki tena! Ila mjijaze Roho! Mwongeleane na kuambiana shangwe na nyimbo na tenzi za Kiroho, mkimwimbia Bwana na kumshangilia mioyoni mwenu, mkamshukuru Mungu Baba po pote kwa ajili yao yote, mliyoyapata katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo! Kisha na mnyenyekeane kila mtu na mwenziwe kwa hivyo, mnavyomwogopa Kristo!* Ninyi wanawake, watiini waume wenu, kama mnavyomtii Bwana! Kwani mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo alivyo kichwa chao wateule, maana yeye ndiye aliyeuokoa mwili. Lakini kama wateule wanavyomtii Kristo, vivyo hivyo nao wake sharti wawatii waume wao katika mambo yote! Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyowapenda wateule, akajitoa mwenyewe kwa ajili yao, awatakase na kuwang'aza akiwaosha maji, kama alivyoagana nao. Ndivyo, alivyotaka kujitengenezea mwenyewe wateule wenye tukuzo hilo la kwamba: Hawanalo doa wala kunjo wala lo lote lifananalo nayo yaliyo hivyo, maana ndio watakatifu pasipo kilema. Ndivyo, inavyowapasa nao waume kuwapenda wake zao, kama ni miili yao. Kwani mwenye kumpenda mkewe hujipenda mwenyewe. Kwani toka kale hakuna mtu ye yote aliyeuchukia mwili wake mwenyewe, ila huulea na kuutunza, kama Kristo naye anavyowafanyia wateule; kwani sisi tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hii mtu atamwacha baba yake na mama yake, agandamiane na mkewe, nao hao wawili watakuwa mwili mmoja. Fumbo hili ni gumu la kulifumbua, lakini mimi nasema la Kristo na la wateule! Lakini hata ninyi kila mmoja wenu na ampende mkewe, kama anavyojipenda mwenyewe! Lakini mke amche mumewe! *Ninyi watoto, watiini wazazi wenu, kwa kuwa mnaye Bwana! Kwani hivi huongoka: Mheshimu baba yako na mama yako! Nalo ni agizo la kwanza lenye kiagio cha kwamba: Upate kukaa vema, nazo siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi! Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu! Ila mwakuze na kuwaonya, wamche Bwana! Ninyi watumwa, kama mnavyomtii Kristo, watiini nao mabwana zenu wa nchini kwa kuwaogopa na kutetemeka, mkilishika mioyoni mwenu lile Neno moja tu! Msifanye kazi nzuri machoni pao tu kama watakao kuwapendeza watu, ila kama watumwa wake Kristo myafanye kwa mioyo, Mungu ayatakayo! Tumikeni na kuuitikia utumishi, kama sio watu, mnaowatumikia, ila kama ni Bwana, mmtumikiaye! Tena mjue: kila mtu akifanya kazi njema yo yote atalipwa naye Bwana, akiwa mtumwa, au akiwa mwungwana. Nanyi mabwana, mwafanyie yaleyale! Mwache kuwatisha mkijua: mbinguni yuko aliye Bwana wao na wenu, tena kwake hakuna upendeleo!* *Mwisho, ndugu zangu, kwa sababu m wake Kristo, mwe wenye kushupaa kwa nguvu ya uwezo wake! Yashikeni mata yote ya Kimungu, mweze kusimama na kuyakinga madanganyo yake msengenyaji! Kwani vita vyetu, tuvipiganavyo, sivyo vya wenye damu na miili, ila ni vya kupigana nao wafalme na wenye uwezo na wenye kutawala nchini penye giza, nao wale pepo wabaya waliopo angani. Kwa hiyo yashikeni mata ya Kimungu yote, mweze kusimama penye mapigano, siku mbaya itakapokuwapo, mpate kuyashinda mabaya yote mkiwa mmesimama vivyo hivyo! Simameni mkiwa mmejifunga ukweli viunoni! Vifuani vaeni wongofu, uwe kanzu yenu ya chuma! Miguuni vaeni viatu! Hivyo mtakuwa tayari kuutangaza utume mwema wa utengemano. Kuliko hayo yote kazeni kumtegemea Mungu, kuwe ngao yenu ya kuizima mishale yote yenye moto ya yule Mbaya! Kichwani vaeni wokovu, uwe kofia yenu ngumu! Kisha shikeni nao upanga wa Kiroho, ndio neno la Mungu!* Tena kwa ajili ya mambo yote mwombe na kubembeleza siku zote kwa nguvu ya Roho! Tena kesheni, myaweze hayo, mkijipingia kuwaombea watakatifu wote! Niombeeni nami, nipate kufumbuliwa kinywa changu, niseme na kulitambulisha waziwazi fumbo la Utume mwema, ambao ninautumikia namo humu kifungoni, nipate kuutangaza pasipo woga, kama inavyonipasa! Lakini kusudi mpate kujua nanyi, mambo yangu yalivyo, nami mwenyewe nilivyo, yote atawasimulia Tikiko aliye ndugu yetu mpendwa na mtumishi mwelekevu wa Bwana. Huyu nimemtuma, aje kwenu kwa ajili hiihii, myatambue, mambo yetu yalivyo, naye aitulize mioyo yenu. Ndugu, mtengemane na kupendana, mpate hata nguvu ya kumtegemea Mungu itokayo kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo! Upole uwakalie wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo pasipo kulegea! Amin. Sisi Paulo na Timoteo tulio watumwa wake Kristo Yesu tunawaandikia ninyi watakatifu nyote mlio naye Kristo Yesu, mkaao huko Filipi, pamoja nanyi watumishi: Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo! *Namshukuru Mungu wangu, kila ninapowakumbuka, kwani kila mara nikiwaombea ninyi nyote ninaomba na kufurahi. Kwani mwashikamana na Utume mwema tangu siku ile ya kwanza mpaka sasa hivi. Kwa hiyo moyo umenitulia, nikijua: Yeye aliyeanza mwenu kazi njema ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu. Ndivyo, inavyonipasa kuwawazia ninyi nyote, kwa sababu ninyi hamtoki moyoni mwangu, ikiwa nafungwa na ikiwa naukania Utume mwema na kuutangaza kwa nguvu; hapo po pote ninyi m wenzangu waliogawiwa kipaji kilekile. Kwani Mungu huona, ninavyowatunukia ninyi nyote kwa hivyo, tulivyo moyoni mwake Yesu Kristo. Neno, niwaombealo, ni hili: upendo wenu uendelee kukua na kuongezeka, kama mlivyoendelea kutambua na kujua maana yote, mpate kuyapambanua yasiyopatana, mtokee siku ya Kristo wenye ung'avu wa mioyo wasiokwaza wengine, mkawa wenye mapato yote ya wongofu, anayotupatia Yesu Kristo, Mungu atukuzwe na kusifiwa.* *Basi, ndugu, nataka, mtambue, ya kuwa mambo yangu yaliyonipata yamegeuka kuwa ya kuuendesha Utume mwema. Maana hapa bomani pote nako kwao wengine minyororo yangu imejulikana, ya kwamba nimefungwa kwa ajili yake Kristo. Tena minyororo yangu imeshikiza ndugu wengi walio wake Bwana, wakajipa mioyo nao ya kulisema Neno la Mungu pasipo woga. Kweli wako wamtangazao Kristo kwa ajili ya wivu na uchokozi, lakini tena wako wanaomtangaza kwa kupendezwa kweli. Hao ndio wanaonipenda, kwani wamejua, ya kuwa nimefungwa, niukanie Utume mwema. Lakini wale humtangaza Kristo, kwamba wanichokoze, lakini mioyo haiwang'ai, maana hutaka kuyaongeza maumivu yangu, niliyo nayo humu kifungoni. Basi, haidhuru; inafaa, Kristo atangazwe tu kwa njia zozote, ikiwa za uwongo, au ikiwa za kweli; kwa hiyo nafurahi. Hata siku zitakazokuja nitafurahi. Kwani najua: hili nalo timizo lake ni wokovu wangu, maana ninyi huniombea, nao Roho wake Kristo hunisaidia. Hiki nacho ni kingojeo changu, nitumikiacho, kitimie: hakuna neno lo lote, ambalo nitatiwa soni nalo, ila kama vilivyokuwa kale, ndivyo, vitakavyokuwa hata sasa: Kristo atatukuzwa waziwazi po pote mwilini mwangu, ikiwa kwa njia ya kuishi au ya kufa. Kwani kwangu mimi kuishi ni Kristo, hata kufa ni kupata.* Lakini kuishi mwilini kunanifaa, niyaone machumo ya kazi yangu; kwa hiyo sikutambui, nitakakokuchagua. Kwani nashindana na haya mambo mawili: ninatunukia kuaga nchini, nipate kuwa pamoja na Kristo; nako ni kuzuri kuliko yote. Lakini kuishi humu mwilini kunafaa zaidi kwa ajili yenu ninyi. Kwa hiyo moyo umenitulia, nikijua, ya kuwa nitakaa nchini, nako kwenu nitakaa nanyi nyote, mwendelee kumtegemea Mungu na kufurahiwa ndiko, majivuno yenu ya kuwa wake Kristo Yesu yaongezeke kwa ajili yangu, mkiniona, nikifika tena kwenu. *Tena neno moja: sharti mwongozane, kama iwapasavyo wenye Utume mwema wa Kristo! Maana ikiwa nafika kwenu, sharti niwaone, au ikiwa niko huku mbali, sharti niwasikie kwamba: Mko mmesimama kwa nguvu ya kutenda roho moja, nayo mioyo ni mmoja tu wa kuja vitani pamoja, mkugombee kuutegemea Utume mwema. Hivyo halitapatikana neno lo lote, wapigani wenu wanaloweza kuwatisha; napo ndipo, wanapojulika kuwa wenye upotevu, nanyi kuwa wenye wokovu, naye mwenye kuwajulisha kuwa hivyo ni Mungu. Kwani ninyi kwa hivyo, mnavyomtumikia Kristo, siko kumtegemea tu mlikopewa, ila mmepewa hata kuteseka kwa ajili yake yeye, mkapatwa na kondo ileile, mliyoiona kwangu kale, tena mnayoisikia, ya kuwa hata sasa ninayo. Hivyo mlivyo naye Kristo, nawabembeleza kwamba: Ikiwa mwatulizana mioyo kwa kupendana, ikiwa m wenye roho moja, au ikiwa m wenye mioyo ya kuoneana uchungu na huruma, ikiwa hivyo, itimilizeni furaha yangu, mawazo yenu yakiwa yayo hayo ya kupendana kila mtu na mwenziwe, mioyo ikiwa mmoja tu wa kulitaka neno lili hili la kwamba: Pasifanyike jambo lolote kwa kuchokozana wala kwa kujitakia majivuno ya bure, ila mnyenyekeane kila mtu akimwazia mwenziwe kuwa mkubwa kuliko yeye! Kila mtu asiyaangalie yaliyo yake tu, ila na ayaangalie nayo yaliyo yake mwenziwe!* *Mioyoni mwenu myawaze yaleyale, Kristo Yesu aliyoyawaza! Yeye alikuwa mwenye sura yake Mungu, tena kule kufanana naye Mungu hakushikamana nako kama ni kitu, alichokiponyoka. Ila alijivua mwenyewe sura ya Kimungu, akajivika sura ya kitumwa, akawa amefanana na watu; walipomtazama, akaonekana, kuwa kama mtu mwenyewe. Akajinyenyekeza mwenyewe, akawa mwenye kutii mpaka kufa, kweli mpaka kufa msalabani. Kwa hiyo naye Mungu alimkweza mbinguni, akampatia Jina lililo kuu kuliko majina yote, maana katika Jina lake Yesu wote wapige magoti, wao walioko mbinguni nao waliopo nchini nao walioko kuzimuni, kila ulimi uungame kwamba: BWANA ni YESU KRISTO; hivyo ndivyo, naye Mungu Baba atakavyotukuzwa.* Wapenzi wangu, kama mlivonitii siku zote, ikiwa niko kwenu, hata ikiwa siko kama siku hizi za sasa: Usumbukieni wokovu wenu wenyewe mkitetemeka kwa kuogopa! Kwani Mungu ndiye aliyewapa kwanza mioyo ya kutaka, kisha ndiye atakaye wapa nako kuyamaliza yampendezayo. Yote yafanyeni pasipo kunung'unika na pasipo kuwaza mengi, mtu asione la kuwaonya, mkiwa wenye hilo Neno moja tu! Hivyo mtakuwa wana wa Mungu wakaao pasipo kilema katikati yao wa ukoo huu wenye uangamizi na upotovu. Katikati yao ndiko, mnakoangaza, kama mianga inavyoangaza ulimwenguni, mkilishika Neno la uzima; hivyo nami nitapata majivuno siku ya Kristo kwamba: Sikupiga mbio bure, wala sikusumbuka bure. Lakini hata nikiuawa kama ng'ombe ya tambiko, ikiwa ya kuwatumikia tu, nafurahi na kuwafurahisha nanyi nyote. Vivi hivi hata ninyi furahini na kunifurahisha nami! Namngojea Bwana Yesu, aitikie, nimtume Timoteo upesi kwenu, moyo wangu upate kutulia ukitambua, mambo yenu yalivyo. Kwani sinaye mtu mwingine, tuliyepatana naye mioyo kama huyu; naye huyasumbukia kweli mambo yenu. Kwani wote huyafuata yaliyo yao; hawayafuati yaliyo yake Kristo Yesu. Lakini yeye mmemtambua, ya kuwa ni mwelekevu, kwani kama mtoto anavyomtumikia baba yake, vivyo hivyo ameitumikia kazi ya kuutangaza Utume mwema pamoja nami. Nangojea, nipate kumtuma yeye; itakuwa papo hapo, nitakapoona, mambo yangu yatakavyotimilika. Hili nalo nalishika moyoni kwamba: Bwana atanipa nami kuja upesi kwenu. Lakini nalishurutishwa moyoni kumtuma Epafurodito kwenu; yeye ni ndugu na mwenzangu wa kazi na wa vita; kisha ni mtume wenu anayenipatia yenye kunitunza. Akawa akiwatunukia ninyi nyote, akasikitika sana, kwa sababu mlikuwa mmesikia, ya kuwa aliugua. Naye alikuwa mgonjwa kweli, kufa kukamfikia. Lakini Mungu akamhurumia, tena siye yeye tu, ila mimi nami, masikitiko yasifuatane kwangu mimi. Kwa hiyo nimemtuma upesiupesi, mpate kuonana naye na kufurahi tena, nami masikitiko yanipungukie. Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana kwa furaha yote! Nao walio hivyo wapeni macheo! Kwani kwa ajili ya kazi ya Kristo alijifikisha kufani, asijitunzie mwenyewe, akitaka kunifanyizia kazi zote za utumishi, ambazo hamkuweza kunifanyizia. Mwisho, ndugu zangu, furahini kuwa wa Bwana! Kuwaandikia ninyi neno lilo hilo moja tu hakunichokeshi, nanyi huwashupaza. Jiangalieni mbwa! Jiangalieni watenda kazi waovu! Jiangalieni nao wanaojikatakata tu! Kwani sisi ndio wenye kutahiriwa tunaomtumikia Mungu rohoni; tunajivunia kuwa wake Kristo Yesu, hatujishikizii mambo ya mwili. Hata mimi kama ningetaka, ningeweza kujishikizia mambo ya mwili, mtu mwingine akijiwazia kuwa na sababu ya kujishikizia mambo ya mwili, mimi namshinda: nilitahiriwa siku ya nane ya kuzaliwa; kabila langu ni Mwisiraeli wa shina la Benyamini, ni Mwebureo mwenyewe, kwa chama cha Maonyo nalikuwa Fariseo, nikajipingia kuwafukuza wateule; hivyo ndivyo, nilivyoutimiza wongofu unaotakwa katika Maonyo, mtu asione la kunionya. Lakini hayo, niliyoyawazia kwamba: Ni mapato, yayo hayo nimeyawazia kwamba: Ni maponzo, maana humzuia Kristo. Kweli nayawazia yote kuwa maponzo, kwani kumtambua Bwana wangu Yesu Kristo ni neno kubwa kuliko yote. Kwa ajili yake yeye niliyaacha yote, kwa kuwa huniponza, nikayawazia kuwa taka, nimpate Kristo tu, nionekane kuwa mwake yeye, maana wongofu wangu utokao penye Maonyo sinao tena, ila wongofu nilio nao ni ule utokao kwa kumtegemea Kristo, ni uleule, mtu anaopewa na Mungu akimtegemea. Huko ndiko kumtambua yeye na nguvu ya ufufuko wake na ya mateso yake, nikiyapata nami kama yeye, hata kufa kwangu kufanane na kufa kwake, nipate kufika kwenye ufufuko katika wafu. Sivisemi hivi kwamba: Nimekwisha kumshika, wala kwamba: nimekwisha kutengenezeka, lakini nakaza mwendo, kwamba nipate kumshika, kama nilivyoshikwa mwenyewe na Kristo Yesu. Ndugu, mimi sijiwazii bado, ya kuwa nimwkisha kumshika. Lakini neno moja nalisema: Yaliyoko nyuma mimi huyasahau, kisha hujipingia yaliyoko mbele. Nakaza mbio, nifike upesi kwenye mwisho wa kushindania, kwenye tunzo lililoko juu kwake Kristo Yesu, nililoitiwa na Mungu. Basi, sote tulio watimilifu tuyafuate mawazo hayo! Kama liko, mwawazalo kuwa jinginejingine, hilo nalo Mungu atawafunulia. Lakini kwanza: hapo, tulipofikia, sharti tupaendelee papo hapo! *Niigeni mimi, ndugu, mwakague wale wanaofanya mwendo kama huu, mnaouona kwetu sisi! Kwani wengi huendelea, kama nilivyowaambia mara nyingi, lakini sasa nawaambia kwa kuwalilia: Ndio wachukivu wa msalaba wake Kristo. Mwisho wao ni kuangamia, mungu wao ni tumbo, utukufu wao umo katika mambo yenye soni, ndio wanaoyawaza tu yaliyopo nchini. Lakini wenyeji wetu uko mbinguni, tunakomtazamia hata mwokozi Yesu Kristo. Yeye ataigeuza miili yetu yenye manyonge, ipate kufanana na mwili wake wenye utukufu kwa hiyo nguvu yake iwezayo kuvishinda vyote, vimtii.* Kwa hiyo, ndugu zangu wapendwa, ninaowatunukia, m furaha yangu na kilemba changu; wapenzi, simameni vivyo hivyo kwake Bwana! Namwonya Ewodia, naye Sintike namwonya, wapatane kwa kuwa wake Bwana. Nawe, mwenzangu wa kweli, nakuomba, uwasaidie wanawake hao, maana waliupigania Utume mwema pamoja nami na pamoja na Klemensi nao wenzangu wengine wa kazi walioandikiwa majina yao katika kitabu cha uzima. *Furahini siku zote kwa kuwa wake Bwana! Nasema tena: Furahini! Utu wenu ujulikane kwao watu wote! Bwana yuko karibu. Msisumbukie kitu! Ila mambo yo yote, myatakayo, mmjulishe Mungu mkimwomba na kumbembeleza pamoja na kumshukuru! Nao utengemano wa Mungu uyapitao yote, tuyatambuayo, uilinde mioyo yenu na mawazo yenu, mkae mwake Kristo Yesu!* Kisha ndugu, yawazeni yote yaliyo yenye kweli nayo yaliyo yenye macheo nayo yaongokayo nayo yang'aayo nayo yapendezayo nayo yaliyo mazuri kusemwa nayo yafaayo kufanywa nayo yo yote yapasayo kusifiwa! Ndiyo, mliyofundishwa, mkayapokea, mkayasikia, mkayaona kwangu mimi; sasa yafanyizeni! Ndipo, Mungu mwenye utengemano atakapokuwa pamoja nanyi. Hivyo, nilivyo mwake Bwana, nalifurahi sana, ya kuwa siku hizi mmekwisha pata tena kunitunza mimi. Tangu kale mlikuwa mkiyawaza, lakini siku za kati hamkuweza. Sisemi hivyo kwamba: Nimekosa kitu. Kwani mimi nimejifunza kutoshewa na hayo, niliyo nayo. Najua kupungukiwa, najua kufurikiwa. Po pote mambo yo yote si mgeni nayo, kama ni kushiba au kuona njaa, kama ni kufurikiwa au kukosa. Nayaweza yote kwa nguvu yake yeye anayenitia nguvu. Lakini mmefanya vizuri mlipojitoa, mwe wenzangu wa maumivu. Nanyi Wafilipi mwajua: tangu hapo, nilipoanza kuutangaza Utume mwema, nilipotoka Makedonia, hakuna wateule wengine walionigawia wakiyatoa yaleyale, waliyopewa, msipokuwa ninyi peke yenu. Hata nilipokuwa Tesalonike, mmetuma mara ya kwanza na mara ya pili, mkanipa vya kunitunza. Sivisemi hivyo kwa maana, nayatafuta matunzo, ila nayatafuta matunda kwamba: Mapato yenu yaongezeke. Kwani nilikuwa nayo yote yanipasayo, nayo yalikuwa mengi. Kisha nikafurikiwa nilipopewa na Epafurodito vitu vile vilivyotoka kwenu; ni manukato yanukayo vizuri kama ng'ombe ya tambiko ifaayo ya kumpendeza Mungu. Mungu wangu awape ninyi, yote mkosayo yawafurikie! Maana yeye ni mwenye mali nyingi zilizomo katika utukufu uliotokea katika Kristo Yesu. Yeye Mungu aliye Baba yetu atukuzwe kale na kale pasipo mwisho! Amin. Nisalimieni kila mtakatifu aliye wake Kristo Yesu! Ndugu walio pamoja nami wanawasalimu. Watakatifu wote wanawasalimu, kupita wengine ni wale waliomo nyumbani mwake Kaisari. Upole wa Bwana wetu Yesu Kristo uzikalie roho zenu! Amin. Mimi Paulo niliye mtume wa Kristo Yesu kwa hayo, Mungu ayatakayo, na ndugu Timoteo tunawaandikia ninyi mlioko Kolose, ndugu watakatifu mnaomtegemea Kristo: Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba yetu! Twamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tunapowaombea ninyi. Kwani tumesikia, mnavyomtegemea Kristo Yesu, tena mnavyowapenda watakatifu wote. Maana mwakishika kingojeo cha yale, mliyowekewa mbinguni; hayo mmeyasikia kale, mlipotangaziwa Utume mwema wa neno la kweli. Nao Utume ulifika kwenu, kama ulivyofika po pote ulimwenguni: huzaa matunda, tena hukua. Vivyo hivyo uko hata kati yenu tangu siku ile, mlipousikia na kuutambua upole wa Mungu kwamba: Ndio wenye kweli. Ndivyo, mlivyofundishwa na Epafura; ni mtumwa mwenzetu mpendwa, tena ni mtumishi mwelekevu wa Kristo anayewafanyizia ninyi kazi. Naye ndiye aliyetueleza, mnavyopendana Rohoni. *Kwa hiyo hata sisi tangu siku ile, tulipoyasikia mambo hayo, hatuachi kumwangukia Mungu na kuwaombea ninyi, mpate kuyatambua yote, ayatakayo, kisha mpewe werevu wote ulio wa kweli na ujuzi wote wa Kiroho. Hivyo mtaweza kuendelea na kumpatia Bwana macheo, apendezwe nanyi kabisa; kisha mtazaa matunda mkizifanya kazi njema zote kwa kuendelea kumtambua Mungu. Tena tunawaombea, mtiwe nguvu zo zote kwa hivyo, utukufu wake ulivyo wenye nguvu, mpate kuyavumilia na kuyanyenyekea yote. Mpate hata kumshukuru Baba kwa furaha, maana amewatengeneza ninyi, mgawiwe fungu la urithi wa watakatifu uliomo mwangani. Yeye ndiye aliyetuokoa katika nguvu ya giza, akatukalisha kwenye ufalme wa mwana wake mpendwa. Mwake yeye ndimo, tupatiamo ukombozi kwa kuondolewa makosa.* Yeye anafanana na Mungu asiyeonekana; ndiye aliyevitangulia viumbe vyote kuzaliwa. Tena ndiye, ambaye vyote viliumbwa mwake yeye, vilivyoko mbinguni navyo vilivyopo nchini, vinavyoonekana navyo visivyoonekana, vikiwa viti vya kifalme au maboma au makao ya wakuu au pengine penye nguvu: vyote pia viliumbwa naye, tena humwelekea. Naye mwenyewe alikuwapo, vitu vyote vilipokuwa havijakuwapo bado, navyo vyote hushikwa naye. Naye mwenyewe ni kichwa cha mwili, maana cha wateule. Naye ni wa kwanza, ni limbuko la wafu, kusudi yeye awe wa kwanza katika mambo yote. Kwani ilimpendeza Mungu, yote pia yamkalie yeye, tena yote yapatanishwe naye, yarudi kwake yeye, kwani hapo, damu yake ilipomwagwa msalabani, ameyapatia utengemano yale yote yaliyopo nchini nayo yaliyopo nchini nayo yaliyoko mbinguni. Hata ninyi kale mlikuwa wageni naye, mkawa hata wachukivu wake, maana mioyoni mlifuata matendo mabaya. Lakini sasa amewapatanisha hata ninyi hapo, alipokufa na kuutoa mwili wake wa kimtu, awageuze nanyi kuwa machoni pake watakatifu pasipo kilema wala kosa. Mtakuwa hivyo mkifuliza kumtegemea, kwani mmajengwa juu ya msingi wenye nguvu, msiwezekane kuondolewa penye kingojeo cha Utume mwema, mliousikia; ndio unaotangaziwa kila kiumbe kilichoko chini ya mbingu. Nami Paulo ninautumikia. Sasa nafurahiwa nayo mateso, niliyoyapata kwa ajili yenu. Nayo maumivu, Kristo aliyoyasaza, nayatimiliza katika mwili wangu, unapoteswa kwa ajili ya mwili wake, maana wateule wake. Ndio wao, niwatumikiao nikiufuata utunzaji wa Mungu, niliopewa, niwatimilizie ninyi Neno lake Mungu. Ni lile fumbo lililokuwa limefichwa tangu kale, baba wasilijue. Lakini sasa watakatifu wake wamekwisha kufumbuliwa; kwani ndio, Mungu aliotaka kuwatambulisha, limbuko likuavyo, lile la utukufu wa fumbo hili, awalimbikialo wamizimu, ndilo hili: Kristo yumo mwenu, yeye ndio utukufu unaongojewa. Naye ndiye, tunayemtangaza sisi, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu werevu wote ulio wa kweli, tupate kumgeuza kila mtu kuwa mtimilifu kwa nguvu ya Kristo. Kazi hii ndiyo, niisumbukiayo na kuishindania kwa uwezo wake yeye anayeniwezesha hivyo kwa nguvu yake. Kwani nataka, mlijue shindano langu kubwa, nililo nalo kwa ajili yenu na ya Walaodikia na kwa ajili yao wote wasioniona uso kwa uso kimwili; nalo ni hili: mioyo yao ipate kutulizwa, ikaunganishwa na kupendana, wapate kuzitwaa nazo mali zote, mtu azipatazo akiwa mwenye ujuzi mwingi, ni kwamba: Nao walitambue fumbo la Mungu na la Kristo. Mwake yeye ndimo, malimbiko yote ya werevu wa kweli na ya utambuzi yalimofichwa. Navisema hivi, mtu asiwadanganye akiwaambia maneno mazuri ya kuwashinda. Kwani mwili ukiwa hauko kwenu, moyo uko pamoja nanyi, ukaning'aa ukiona, mwonyekavyo, tena mjishupazavyo kumtegemea Kristo. Basi, kama mlivyompokea Bwana Kristo Yesu, hivyo mwendelee kuwa wake, mkishusha mizizi mumo humo mwake, mkajengwa mlemle na kuongezwa nguvu za kumtegemea, kama mlivyofundishwa; hivyo mtayavumisha yale mema, mliyogawiwa. Mjiangalie, mtu asije, akawateka akiwafundisha maneno ya ujuzi yaliyo ya udanganyi wa bure tu, hufanana na masimulio ya watu kama ya mambo yaliyo ya kwanza humu ulimwenguni, lakini siyo ya Kikristo. Kwani mwake Kristo ndimo mkaamo kimwili wingi wao yote yaliyo ya Kimungu. Nanyi mkiwa naye huyapata hayo yote, maana yeye ni kichwa cha kila ukuu na cha kila nguvu. Tena mkiwa naye yeye hutahiriwa pasipo kutumia mikono ya mtu, maana huuvua mwili wa kimtu ulio wenye makosa, ndiko kutahiriwa Kikristo. Hapo, mlipobatizwa mmezikwa pamoja naye, tena papo hapo mmefufuliwa pamoja naye kwa nguvu ya kumtegemea, mwipatayo kwake, Mungu aliyemfufua katika wafu. Nanyi mlikuwa wenye kufa kwa ajili ya makosa, nayo miili yenu ilikuwa haikutahiriwa hivyo, lakini aliwapa kuishi pamoja naye, akawaondolea makosa yote. Kisha akakifuta cheti kilichoandikwa maagizo, tusiyoyashika, ndicho kilichotusuta; akakiondoa hapo kati, akakipigilia msalabani. Nao wakuu wa wangavu akawavua ukuu wao na nguvu zao, akaonyesha waziwazi, walivyo, akawatembeza kama mateka. Kwa hiyo mtu asiwaumbue kwa ajili ya kula au kunywa, wala kwa ajili ya kuacha kuzipa cheo sikukuu zo zote, ikiwa za miandamo ya mwezi au za mapumziko. Mambo hayo ni kivuli tu cha mambo yaliyotaka kutokea, lakini yametimia kimwili, Kristo alipokuja. Mtu asiwanyang'anye tunzo lenu akiwataka, mfuatane naye kujinyenyekeza na kuwatambikia malaika! Hujiwazia kwamba: Yako, aliyoyaona, kisha hujikazia yayo hayo akijitutumua bure kwa mawazo ya mwili wake, asishikamane naye aliye kichwa, aliye mwenye kuuunganisha mwili wote, ukitiwa nguvu kwa fundo na viungo, upate kumkulia Mungu. Kama mmekufa pamoja naye Kristo mkiyaacha yale mambo yaliyo ya kwanza humu ulimwenguni, kwa nini mwataka tena kupewa miiko kama wenye kuukalia ulimwengu huu? Mwaambiwa: Usivishike! wala: Usivionje! wala: Usiviguse hivi na hivi! Navyo vyote vimewekwa, vitumike, kisha vioze. Kwa hiyo yale maagizo na mafundisho ni ya kimtu tu; kweli watu husema: Ni ya werevu wa kweli, wakiyachagua matumizi yao ya Mungu na unyenyekevu wao, tena wakiinyima miili yao yaipasayo, lakini yote ni kazi za bure tu, maana zikiisha, huzitimiza tamaa zote za miili. *Basi, kama mmefufuka pamoja naye Kristo, yatafuteni yaliyoko juu! Ndiko, Kristo akaako kuumeni kwa Mungu. Yawazeni yaliyoko juu, msiyawaze yaliyopo nchini! Kwani mmekufa, lakini uzima wenu uko umefichwa pamoja na Kristo kwake Mungu. Hapo Kristo aliye uzima wenu atakapofunuliwa, ndipo, nanyi mtakapofunuliwa pamoja naye kuwa wenye utukufu.* Basi, viueni viungo viyatimizavyo yaliyopo nchini: ugoni na uchafu na tamaa na kijicho kiovu na choyo kilicho sawa na kutambikia vinyago! Kwa ajili ya mambo hayo makali ya Mungu hutokea. Nanyi mambo hayo mliandamana nayo hapo kale, mlipokuwa mkiyakalia. Lakini sasa nanyi hayo yote sharti myatoke: makali na mifundo ya mioyo na maovu na matusi na mateto mabaya yaliyomo vinywani mwenu. Msiambiane yaliyo ya uwongo! Mvueni mtu wenu wa kale pamoja na matendo yake! Mvaeni yule mtu mpya apataye upya kwamba: Katika utambuzi afanane naye aliyemwumba! Hapo hapana tena Mgriki na Myuda, wala aliyetahiriwa na mwingine asiyetahiriwa, wala mgeni na mshenzi, wala mtumwa na mwungwana. Ila Kristo ndiye yote, naye yumo mwao wote. *Ninyi watakatifu na wapendwa, kwa hivyo, mlivyochaguliwa na Mungu, vaeni mioyo yenye huruma za kweli na utu na unyenyekevu na upole na uvumilivu! Mvumiliane ninyi kwa ninyi na kuachiliana, mtu akiwa na neno la kumkamia mwenziwe! Kama naye Bwana alivyowaachilia ninyi, vivyo hivyo vifanyeni nanyi! Lakini lililo kuu kuliko haya yote: uvaeni upendano! Maana ndio unaoyatimiza yote na kutupatanisha kuwa mmoja. Nao utengemano wa Kristo utawale mioyoni mwenu! Kwani ndio, mlioitiwa, maana m mwili mmoja. Tena mema, mliyogawiwa, myavumishe! Neno la Kristo likae mwenu, kama ni mali, mzikaliazo, mkifundishana pamoja na kuonyana na kujulishana ujuzi wote, mmwimbie Mungu mioyoni mwenu shangwe na nyimbo na tenzi za Kiroho za kwamba: Tumegawiwa mema! Nayo yote, mtakayoyatenda, ikiwa maneno ya kusema au kazi za kufanya, yafanyeni yote katika Jina la Bwana Yesu mkimvumisha Mungu Baba kwa kufanya hivyo!* Ninyi wake, watiini waume wenu, kama inavyowapasa walio wa Bwana! Ninyi waume, wapendeni wake zenu, msiwaendee kwa ukali! Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote! Kwani hivi vinampendea Bwana. Ninyi baba, msiwachokoze watoto wenu, wasishindwe na kutii! Ninyi watumwa, katika mambo yote watiini walio mabwana zenu kimtu! Msiwatumikie hapo machoni tu, kama wenye kupendeza watu, ila kama wenye kumwogopa Bwana watumikieni kwa mioyo iliyo na neno moja tu! Katika yote, mnayoyatenda, zifanyeni kazi zenu kwa mioyo, kama ni kazi zinazofanyiziwa Bwana, zisizofanyiziwa watu! Jueni, ya kuwa mtapokea kwake Bwana malipo hapo, mtakapoupata urithi wenu! Mtumikieni Bwana Kristo! Lakini mpotovu atayatwaa mapato yao yale, aliyoyapotoa, lakini hakuna upendeleo. Ninyi mabwana, wapeni watumwa wenu yawapasayo, mwalinganishe! Jueni, nanyi mko na Bwana mbinguni! Fulizeni kumwomba Mungu! Kesheni kuomba na kushukuru! Na sisi vilevile tuombeeni, Mungu atufungulie mlango wa kuingizamo Neno lake, tupate kulisema fumbo la Kristo, ni lilelile, nililofungiwa, nipate kulifumbua, kama inavonipasa kulisema! Walioko nje waendeeni kwa werevu wa kweli! Siku mlizopewa, mzitumie vema! Maneno yenu yawe po pote ya kupendeza yakiwa matamu kama yenye chumvi, mpate kujua yanayofaa ya kumjibu mtu awaye yote! Mambo yangu yote yalivyo, atawatambulisha Tikiko aliye ndugu mpendwa na mtumishi mwelekevu na mtumwa mwenzangu, kwa kuwa wake Bwana. Nami nimemtuma kwenu kwa ajili ya neno lili hili, mpate kuyatambua mambo yetu, naye ataituliza mioyo yenu. Anaye Onesimo, ni ndugu mwelekevu, nimpendaye, ni mtu wa kwenu. Watawatambulisha, yote ya huku yalivyo. Aristarko, mfungwa mwenzangu, na Marko, mpwae Barnaba, wanawasalimu ninyi; kwa ajili yake yeye mmepata maagizo; atakapokuja kwenu, mpokeeni! Naye Yesu anayeitwa Yusto anawasalimu. Kwao Wakristo wa Kiyuda ni hao watatu tu walio wenzangu wa kazi ya kuujenga ufalme wa Mungu, ndio walionituliza moyo. Epafura aliye wa kwenu anawasalimu; ni mtumwa wa Kristo Yesu, naye huwagombea kila siku na kuwaombea, mpate kusimama wenye kuyatimiza na kuyatambua yote, Mungu ayatakayo. Kwani namshuhudia kwamba: Hujisumbua sana kwa ajili yenu na kwa ajili yao walioko Laodikia na Hierapoli. Luka aliye mganga mpendwa na Dema wanawasalimu. Wasalimieni ndugu walioko Laodikia, naye Nimfa nao wateule waliomo nyumbani mwake! Barua hii, ikiisha kusomwa kwenu, angalieni, isomwe hata kwao wateule wa Laodikia, nanyi mwisome ile ya Laodikia! Tena mwambieni Arkipo: Uangalie utumishi wako, ulioupokea wa kumtumikia Bwana, uutimize vema! Salamu hii naiandika kwa mkono wangu mimi Paulo. Ikumbukeni hii minyororo yangu! Upole uwakalie! Amin. Sisi Paulo na Silwano na Timoteo tunawaandikia ninyi mlio wateule wa Tesalonike katika Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo. Upole uwakalie na utengemano! Tunamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu nyote. Nasi hatuachi kuwakumbuka katika kuomba kwetu tukikumbuka mbele ya Mungu aliye Baba yetu, mnavyofanya kazi kwa kumtegemea, tena mnavyojisumbua, mpate kupendana, tena mnavyovumilia na kumngojea Bwana wetu Yesu Kristo. Kwani ndugu mliopendwa na Mungu, twajua: mmechaguliwa. Kwani Utume wetu mwema haukuwa kwenu katika maneno tu, ila ulitenda hata nguvu, ukawapo nayo Roho takatifu, mkapata pa kujishikizia sana; mwajua, tulivyokuwa kwenu kwa ajili yenu. Nanyi mkatuiga sisi naye Bwana; mlikuwa na maumivu mengi, mkalipokea Neno kwa furaha, watu wapewayo na Roho takatifu. Kwa hiyo wote wamtegemeao Mungu katika nchi ya Makedonia na ya Akea waliweza kujifundishia kwenu ninyi. Kwani uvumi wa Neno la Bwana ulitoka kwenu, ukaenea Makedonia na Akea, lakini si huko tu, ila imejulikana waziwazi po pote, mnavyomtegemea Mungu. Kwa hiyo haitupasi sisi kuvisema mahali po pote, kwani wenyewe huvisimuliana, mlivyotupokea, tulipoingia kwenu, nanyi mlivyomgeukia Mungu mkaviacha vinyago vya kutambikia, mpate kumtumikia Mungu aliye mwenye uzima na ukweli, tena mnavyomgojea Mwana wake, atoke mbinguni; ni yeye Yesu, aliyemfufua katika wafu, naye ndiye atakayetuokoa katika makali yatakayokuja. Ndugu, mwajua wenyewe, tulivyoingia kwenu, ya kuwa hatukuingia bure. Huko Filipi, tulipoanzia, tuliumizwa na kukorofishwa vibaya, kama mnavyojua; lakini Mungu wetu akatupa mioyo ya kuwatangazia Utume mwema wa Mumgu pasipo woga wo wote na kuushindania sana. Kwani yale, tuliyowaonya, siyo ya kuwapoteza wala ya kuwapeleka penye uchafu wala ya kuwadanganya. Ila kama tulivyojulika kwake Mungu kuwa wakweli wapaswao na kupewa Utume mwema, hivyo ndivyo, twasemavyo, siko kwamba tupendeze watu, ila tumpendeze Mungu ajulishaye, mioyo yetu ilivyo. Kwani hatukutumia maneno matamutamu ya kujipendezesha kwenu, kama mnavyojua, wala hatukujitendekeza kama wenye kuficha choyo; hapa Mungu ndiye anayetushuhudia. Wala hatukutaka kutukuzwa na watu, wala nanyi wala na watu wengine. Tuliweza kuwa wenye macheo, maana tu mitume wake Kristo, lakini kati yenu tulikuwa wenye upole, kama mlezi akiwalea watoto wake. Vivyo hivyo na sisi tuliwatunukia ninyi, tukataka sana kuwagawia Utume mwema wa Mungu, hata mioyo yetu nayo, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu. Ndugu, mwayakumbuka masumbuko na maumivu yetu: tuliutangaza Utume mwema wa Mungu kwenu na kufanya kazi usiku na mchana, tukikataa kumlemea mtu wo wote wa kwenu. Ninyi pamoja na Mungu m mashahidi, jinsi tulivyowaendea ninyi mmtegemeao, maana tulikuwa wenye kumcha Mungu na wenye wongofu, mtu asione la kutuonya. Hilo nalo mwalijua: kama baba anavyowabembeleza watoto wake, vivyo hivyo tumewabembeleza ninyi kila mmoja wenu peke yake; tukawatuliza mioyo pamoja na kuwakaza, mfanye mwenendo uwapasao walio wake Mungu aliyewaitia ninyi kuuingia ufalme na utukufu wake. Kwa sababu hii na sisi hatukomi kumshukuru Mungu kwamba: Mlipolisikia kwetu Neno lake Mungu mmelipokea si kama neno la watu, ila kama Neno lake Mungu, lilivyo kweli. Naye ndiye anayetenda nguvu mwenu mmtegemeao. Kwani ninyi ndugu, mmepata kufanana na wateule wa Mungu walio wake Kristo Yesu katika nchi ya Yudea, kwani nanyi mmeteswa yaleyale na wenzenu wa kabila, kama nao wale walivyoteswa na Wayuda. Ndio wao hao waliomwua naye Bwana Yesu, hata wafumbuaji, tena ndio waliotufukuza na sisi; hawampendezi Mungu kwa kupingana na watu wote. Kisha hujaribu kutukataza sisi, tusiwaambie wamizimu Neno la wokovu wao; hivyo huyatimiza makosa yao po pote. Lakini makali yamewafikia, waishie. Sisi ndugu tumetengwa nanyi kitambo cha sasa, tusionane nanyi uso kwa uso, lakini mioyo haikutengwa; kwa hiyo tulijipingia sana kuonana nanyi uso kwa uso, kwani tuliwatunukia sana. Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, mimi Paulo nilitaka mara moja, hata mara mbili, lakini Satani alituzuia. Kwani kingojeo chetu au furaha yetu au kilemba, tujivuniacho mbele ya Bwana wetu Yesu Kristo, atakapokuja, ndio nini, msipokuwa ninyi? Kwani ninyi m utukufu wetu na furaha yetu. Kwa hiyo hatukuweza kuvumilia tena, tukapendezwa kuachwa peke yetu huko Atene, tukamtuma ndugu yetu Timoteo anayemtumikia Mungu na kuutangaza Utume mwema wa Kristo; tulimtuma, awashupaze ninyi na kuwatuliza mioyo kwa hivyo, mnavyomtegemea Mungu, mtu asitikisike katika maumivu ya siku hizi; kwani mwajua wenyewe: jambo tulilowekewa, ni hilo. Kwani hata hapo, tulipokuwa kwenu, tuliwafumbulia kwamba: Inatupasa kuumizwa; ndivyo vilivyotimia sasa, kama mnavyojua. Kwa hiyo nami sikuweza kuvumilia tena, nikamtuma, nipate kutambua, kama mwamtegemea Mungu bado, au kama yule mwenye kujaribu amewajaribu, masumbuko yetu ya kwenu yakawa ya bure. Lakini sasa Timoteo amefika kwetu kutoka kwenu, akatusimulia vema mambo mema, mnavyomtegemea Mungu, mnavyopendana, mnavyotukumbuka vema siku zote mkitunukia kutuona sisi, kama sisi tunavyotunukia kuwaona ninyi. Kwa hayo, ndugu, tumetulizwa mioyo kwa ajili yenu katika mahangaiko na maumivu yetu yote, tuliposikia, mnavyomtegemea Mungu. Kwani sasa tumerudi uzimani tena, ikiwa ninyi mmesimama penye Bwana. Kwa shukrani gani, tutakazomtolea Mungu kwa ajili yenu, tutaweza kumlipa furaha zote, tulizozipata kwenu mbele yake yeye Mungu wetu? Nasi twafuliza kuomba sanasana usiku na mchana, tupate kuonana nanyi uso kwa uso, tuweze kuziongeza nguvu zenu za kumtegemea Mungu, pakiwapo zilipokoseka. Yeye Mungu aliye Baba yetu naye Bwana wetu Kristo na atuongoze njia ya kufika kwenu! Ninyi Bwana awaongezee upendano, mfurikiwe nao, mpate kupendana ninyi kwa ninyi, kisha mwapende nao wote wengine, kama sisi nasi tunavyowapenda ninyi! Hivyo mioyo yenu itashupaa, tena haitakosa kutakata kwa kuwa haina madoadoa, Mungu aliye Baba yetu akiitazama hapo, Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na watakatifu wake wote. *Pamesalia, ndugu, tuwahimize na kuwabembeleza, kwa hivyo, mlivyo wake Bwana Yesu, mfanye mwenendo uwapasao wa kumpendeza Mungu ulivyo. Kwani mwayajua maagizo, tuliyowaagiza, kama tulivyoyapata kwake Bwana Yesu. Kwani haya ndiyo, Mungu ayatakayo: mtakaswe, mwuepuke ugoni. Kila mmoja wenu ajue kuuangalia mwili wake, uwepo ukitakata na kupata heshima iupasayo, usivurugikane na tamaa na kijicho, kama wamizimu walivyofanya, wasiomjua Mungu! Katika jambo hili mtu asiupite mpaka akimdanganya ndugu yake, kwani Bwana ndiye atakayeyalipizia hayo yote, kama tulivyowaambia kale na kuwashuhudia. Kwani Mungu hakutuitia kuwa wenye uchafu, ila tuje, tutakaswe. Basi, kwa hiyo mtu akiyatangua haya, hatangui ya mtu, ila yake Mungu aliyewapa ninyi Roho wake Mtakatifu, awakalie. Kwa ajili ya upendano ninyi hampaswi na kuandikiwa neno, kwani ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. Nanyi mnawafanyia hivi ndugu wote katika nchi yote ya Makedonia. Lakini twawaonya ninyi, ndugu, lifulizieni jambo hili! Uchuchumieni utulivu, mpate kuyafuata mambo yenu wenyewe na kufanya kazi kwa mikono yenu, kama tulivyowaagiza! Sharti mfanye mwenendo uwafaliao wale watu wa nje, kwao msitake mtu wo wote wa kuwasaidia.* *Lakini, ndugu, hatutaki, ninyi mkose kujua, mambo yao waliolala yalivyo, msione masikitiko kama wale wengine wasio na kingojeo. Kwani tukiyategemea, ya kuwa Yesu alikufa, kisha akafufuka tena, vivyo hivyo Mungu nao waliolala katika Yesu atawapeleka, wawe pamoja naye. Kwani neno hili, tunalowaambia, ni neno lake Bwana kwamba: Sisi tunaoishi, tuliosazwa, mpaka Bwana atakapokuja, hatutawatangulia wale waliolala. Kwani Bwana mwenyewe atashuka toka mbinguni papo hapo, wito utakapovumika, nayo sauti ya malaika mkuu itasikilika, hata baragumu la Mungu litalia. Ndipo, waliokufa katika Kristo watakapofufuka kwanza; kisha sisi tuliosazwa, tutakaokuwa tu hai, tutapokonywa katika mawingu pamoja nao hao, tupate kukutana na Bwana angani. Hivyo tutakuwa pamoja na Bwana siku zote. Tulizaneni mioyo ninyi kwa ninyi na kisimuliana maneno haya!* Ndugu, hampaswi na kuandikiwa, kama itakuwa mwaka gani au siku gani, hayo yatakapokuwapo. Kwani wenyewe mwajua sana: siku ya Bwana itafika, kama mwizi anavyokuja usiku. Watakaposema: Pametengemana, pametulia, ndipo, watakapogunduliwa na mwangamizo, kama uchungu wa kuzaa unavyompata mwenye mimba; kwa hiyo hawataweza kukimbia. Lakini ninyi, ndugu, hammo gizani, kwa hiyo siku ile hitawafumania kama mwizi. Kwani ninyi wote ni wana wa mwanga na wana wa mchana; sisi hatu wa usiku, wala wa giza. Kwa sababu hii tusilale usingizi, kama wale wengine wanavyolala usingizi, ila tukeshe na kulevuka! Kwani wanaolala usingizi hulala usiku, nao wanaolewa hulewa usiku. Lakini sisi tulio wa mchana tulevuke! Kisha tujivike mata: kumtegemea Mungu na kupendana kuwe kanzu zetu za chuma, nako kuungojea wokovu kuwe kofia zetu ngumu. Kwani Mungu hakutuweka, tuishie kwa makali yake, ila alituweka, tuupate wokovu kwa kazi ya Bwana wetu Yesu Kristo aliyekufa kwa ajili yetu sisi, tupate kuishi pamoja naye yeye, tukiwa tuko macho, au tukiwa tumelala usingizi. Kwa hiyo mtulizane na kujengana kila mmoja na mwenzake, kama mnavyofanya! Ndugu, twawaomba sana, mwajue wale wanaojisumbua kwenu ninyi wakiwasimamia, mkae naye Bwana, tena wakiwaonya. Jipigieni sana kuwapa macheo na kuwapenda kwa ajili ya kazi yao! Pataneni ninyi kwa ninyi! *Lakini twawahimiza ninyi, ndugu: Waaonyeni wenye mambo ya ovyo tu, watulizeni wenye mioyo miepesi, wasaidieni wanyonge, wo wote waendeeni kwa uvumilivu! Mwangalie, mtu asimlipe mwenziwe uovu kwa uovu! Ila siku zote myafuate yaliyo mema, myapatiane ninyi kwa ninyi, hata wengine wote! Changamkeni siku zote! Mwombeni Mungu pasipo kukoma! Katika mambo yote toeni shukrani! Kwani haya ndiyo, Mungu ayatakayo, myafanye, kwa kuwa wake Kristo Yesu. Roho msimzime! Mafumbuo msiyabeze! Ila yote yapambanueni, kisha lishikeni lililo jema! Yote yaonekanayo kuwa mabaya yaepukeni! Lakini yeye Mungu aliye mwenye utengemano awatakase ninyi nyote miili na mioyo, kwamba roho zenu zote nzima pamoja na mioyo na miili zilindwe, zikae pasipo doadoa lo lote, mpaka Bwana wetu Yesu Kristo atakaporudi! Naye aliyewaita ni mwelekevu, naye ndiye atakayeyafanya.* Ndugu, tuombeeni kwake Mungu! Wasalimuni ndugu wote na kunoneana, kama watakatifu walivyozoea! Nawaapisha ninyi kwa Bwana, barua hii isomewe ndugu wote. Upole wa Bwana wetu Yesu Kristo uwakalie! Amin. Sisi Paulo na Silwano na Timoteo tunawaandikia ninyi mlio wateule wa Tesalonike katika Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo! Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo! *Sharti tumshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu, ndugu; hii inatupasa, kwa sababu nguvu zenu za kumtegemea Mungu zinaongezeka sana, nao upendano unakua, maana ninyi nyote kila mmoja wenu humpenda mwenzake. Kwa hiyo hata sisi wenyewe twajivuna kwa ajili yenu katika wateule wa Mungu, kwamba mwavumilia, tena mwamtegemea Bwana katika mafukuzo na maumivu yenu yote, mnayojitwika. Humu ndimo, hukumu yake Mungu itakamoonekana kuwa ya kuongoka: ninyi mtaambiwa: Ufalme wa Mungu umewapasa kwa hivyo, mnavyoteswa kwa ajili yake huo. Kwani wongofu wa Kimungu ndio huu: wenye kuwaumiza atawalipizia maumivu, nanyi mwumizwao mtapata kutulizwa pamoja nasi, Bwana Yesu atakapotokea waziwazi toka mbinguni pamoja na malaika wa nguvu zake. Naye atashuka mwenye moto uwakao sana, awalipize wale wasiomjua Mungu, kwamba walikataa kuutii Utume mwema wa Bwana wetu Yesu. Nalo lipizi, watakalolipata, ni mwangamizo wa kale na kale, maana watatupwa, wasiuone uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake. Hivi vitakuwa siku ileile, atakapokuja kutukuzwa kati ya watakatifu wake na kustaajabiwa kati yao wote wamtegemeao; kwani mambo hayo, tuliyoyashuhudia, yalipata kwenu wenye kuyategemea.* Kwa ajili ya neno hili twawaombea ninyi siku zote, Mungu wetu awape kufanya mwenendo uupasao wito wenu, mpate nguvu za kuyatimiza mema yote yaliyowapendeza na za kufanya matendo yafanyikayo kwa kumtegemea. Hivyo ndivyo, Jina la Bwana wetu Yesu litakavyotukuzwa mwenu, nanyi mtatukuzwa mwake, yatakapotimia yale, Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo aliyowagawia. Ndugu, kwa ajili ya kurudi kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kwa ajili ya kwamba: Sisi tutakusanyika kwake, tunawaomba sana ninyi, msitetemeshwe upesi mkipotelewa na njia, wala msihangaike mkisikia mambo ya kirohoroho au ya masimulio au ya barua, ya kuwa neno limetoka kwetu la kwamba: Siku ya Bwana imekwisha fika! Mtu asiwadanganye na kuwaongoza katika njia, iwayo yote! Kwani sharti kwanza matanguo yaje, naye yule mtu wa upotovu sharti ajulishwe kuwa mwana wa mwangamizo, ni mbishi, ni mwenye kujikweza kuwa mkuu kuliko yote yaitwayo Mungu au tambiko, mpaka akija kukaa katika Jumba la Mungu na kutangaza: Mungu ni mimi! Hamkumbuki, ya kuwa niliwaambia hayo nilipokuwa kwenu? Nacho kinachomzuia sasa mwakijua; lakini siku yake itakapotimia, atatokea waziwazi. Kwani ule upotovu uliokuwa umefichwa umekwisha anza kutenda nguvu, kisaacho ni hiki: yule mwenye kuuzuia mpaka sasa sharti aondolewe, atoke hapo kati. Kisha ndipo, yule mpotovu atakapofunuliwa. Naye Bwana Yesu atamwua akimpuzia tu kwa kinywa chake, atenguke kwa mwangaza wa kuja kwake. Lakini yule mpotovu uwezo wa kuja kwake ni ule wa Satani, ukamfanyisha ya nguvu yo yote na vielekezo na vioja vya uwongo, nao wenye kuangamia huwaponza kwa udanganyi wo wote, kwa sababu waliyakataa yaliyo ya kweli, wasiyapende, wapate kuokolewa. Kwa sababu hiyo Mungu anawaletea mapotevu yenye nguvu, wayategemee yaliyo ya uwongo, wapate kuhukumiwa wote wasioyategemea yaliyo ya kweli, ila walipendezwa nayo yaliyo ya upotovu. Ndugu, sisi imetupasa kumshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu mliopendwa na Bwana, maana Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo, mpate wokovu mkitakaswa roho, mkayategemea yaliyo ya kweli. Haya ndiyo, aliyowaitia, tulipowatangazia Utume mwema, mpate kuuchuma utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu, sasa simameni na kuyashika mafundisho, mliyofundishwa nasi, ikiwa mliambiwa au mliandikiwa! Lakini yeye, Bwana wetu Yesu Kristo, na Mungu Baba yetu aliyetupenda sisi, akatugawia kwa upole wake matulizo yaliyo ya kale na kale na kingojeo chema, awatulize mioyo yenu na kuitia nguvu, myafuate matendo na mambo yote yaliyo mema! Kisha, ndugu, mtuombee sisi kwa Mungu, Neno la Bwana liendelee na kutukuzwa vivyo hivyo kama kwenu! Tena tuombeeni, tuokolewe mikononi mwa watu walio wapuzi na wabaya! Kwani sio wote wawezao kumtegemea Bwana. Lakini Bwana ni mwelekevu atakayewashupaza na kuwalinda, yule Mbaya asiwajie. Kwa ajili yenu tunamtumaini Bwana kwamba: Tunayowaagiza, mwayashika sasa, hata siku za nyuma mtayashika. Bwana aiongoze mioyo yenu, iufikie upendo wa Mungu na uvumilivu wa Kristo! *Ndugu, tunawaagiza ninyi, kwa nguvu ya Jina la Bwana Yesu Kristo, mtengane na kila ndugu anayeendelea na kufuata mambo yaliyo ya ovyoovyo tu, asiufuate ufundisho, mlioupata kwetu sisi. Kwani mwajua wenyewe, jinsi inavyowapasa kutuiga, kwa sababu hatukukaa kwenu kiovyoovyo tu. Hakuna, ambaye tulikula chakula chake bure, ila tulijisumbua na kujiumiza tukifanya kazi usiku na mchana kwa kukataa kumlemea mtu ye yote wa kwenu. Hatukuvifanya hivyo kwamba: Hatu wakuu, ila tulitaka kuwapa ninyi vielezo, mpate kutuiga. Kwani tulipokuwa kwenu tuliwaagiza hata neno hili: Mtu asiyetaka kufanya kazi asipate chakula! Kwani twasikia: Kwenu wako wanaoendelea na kufuata mambo yaliyo ya ovyoovyo tu, hawafanyi kazi, ila hufanya mapuzi. Walio hivyo tunawaagiza na kuwaonya machoni pake Bwana Yesu Kristo, watulie, wapate kufanya kazi na kula chakula chao wenyewe. Lakini ninyi, ndugu, msichoke kufanya yaliyo mazuri!* Lakini mtu asipoyatii maneno yetu yaliyomo humu baruani, huyo mjulisheni mkikataa kuchanganika naye, apatwe na soni! Lakini msimwazie kuwa mchukivu, ila mwonyeni kindugu! Lakini yeye Bwana aliye mwenye utangemano awape kutengemana po pote katika mambo yote! Bwana awe nanyi nyote! Salamu hii naiandika kwa mkono wangu mimi Paulo; huu ndio mwandiko wangu katika barua zote. Hivi ndivyo, ninavyoandika. Upole wa Bwana wetu Yesu Kristo uwakalie ninyi nyote! Amin. Mimi Paulo niliye mtume wa Kristo Yesu kwa agizo lake Mungu aliye mwokozi wetu na kwa agizo lake Kristo Yesu aliye kingojeo chetu nakuandikia, wewe Timoteo uliye mwanangu wa kweli kwa hivyo, unavyomtegemea Mungu. Upole ukukalie na huruma na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba na kwa Bwana wetu Kristo Yesu! Hapo, nilipokwenda Makedonia nilikuagiza wewe kukaa Efeso, uwakataze wengine, wasifundishe menginemengine, wala wasishikamane na masimulio yasiyo ya kweli wala na mambo ya mashina ya koo za kale yasiyokoma. Haya huleta mabishano, lakini hayaufalii utunzaji wa Mungu wa kuwatunza wenye kumtegemea. Lakini agizo hilo linatimia, wakipendana kwa mioyo itakatayo, ijuayo yaliyo mema tu, imtegemeayo Mungu kwa kweli pasipo ujanja. Wengine wameikosa mioyo iliyo hivyo, wakapotelea katika maneno ya upuzi; walitaka kuwa wafunzi wa Maonyo, lakini hawajui, wala wasemayo, wala wabishayo. Twajua, ya kuwa maonyo ni mazuri, mtu akiyatumia kujionya kwa kujua kwamba: Mwongofu siye aliyetolewa Maonyo, ila waliotolewa ndio wapotovu nao wasiotii nao wasiomcha Mungu nao wakosaji nao wachafu nao wabezi nao wauao baba zao nao wauao mama zao nao wauao wenzao nao wagoni nao walalanao nao wauzao watu nao waongo nao waapao viapo vya uwongo, na kama wako wengine wafanyao neno jingine lisilopatana na ufundisho uwapao watu uzima. Hivyo ndivyo, tulivyofundishwa na Utume mwema wa utukufu wake Mungu anayeshangiliwa; nami nimepewa kuutangaza. Namshukuru Bwana wetu Kristo Yesu aliyenitia nguvu, akaniona kuwa mwelekevu, akanipa utumishi mimi niliyekuwa kale mwenye kuwatukana na kuwafukuza na kuwakorofisha walio wake. Lakini nilihurumiwa, kwani naliyafanya pasipo kujua maana, kwani nilikuwa sijamtegemea Bwana. Lakini mema, Bwana wetu aliyonigawia, yakawa mengi mno, nikapata kwake Kristo Yesu kumtegemea na kumpenda. Neno hili ni la kweli, nalo linapasa kushikwa na watu wote la kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wakosaji, ambao mimi ni wa kwanza wao, lakini nilihurumiwa, kusudi Kristo Yesu aonyeshe kwanza kwangu mimi uvumilivu wote, niwe kielezo chao watakaomtegemea, waupate uzima wa kale na kale. Mungu aliye peke yake mfalme wa kale na kale, asiye na kikomo, asiyeonwa na macho ya watu, aheshimiwe na kutukuzwa kale na kale pasipo mwisho! Amin.* Mwanangu Timoteo, kwa ajili ya maneno ya ufumbuaji, uliyosemewa kale, nakupa agizo hili, uyashindanie mashindano mazuri ukiwa mwenye kumtegemea Mungu na wenye moyo ujuayo yaliyo mema tu. Wengine waliutupa moyo ulio hivyo, kwa hiyo nazo nguvu zao za kumtegemea Mungu zikatota; miongoni mwao wamo Himeneo na Alekisandro; hawa nimewatoa, Satani awashike, waonyeke, wasimbeze Mungu tena. *Neno, ninalokuhimiza kupita yote, ni hili: Mwombe na kumwangukia Mungu na kumbembeleza na kumshukuru mkiwaombea watu wote, nao wafalme nao wote walio wakuu, tupate kukaa tukitulia na kutengemana vema, tumche Mungu na kuendelea vema katika mambo yote. Kwani hivi ni vizuri vya kumpendeza Mungu, mwokozi wetu. Huyu anataka, watu wote waokolewe, wapate kutambua yaliyo ya kweli. Kwani Mungu ni mmoja, naye mpatanishaji wa Mungu na watu ni mmoja, ni yule mtu Kristo Yesu aliyejitoa mwenyewe kuwa kole ya kuwakomboa wote; huu ndio ushuhuda utakaotangazwa po pote, siku zake zitakapotimia.* Nami nimewekewa kuwa mtangazaji na mtume wake, nasema kweli, sisemi uwongo, niwe mfunzi wa wamizimu, niwafundishe kumtegemea Mungu na kuyashika yaliyo ya kweli. Nataka, waume wamwombe Mungu mahali pote wakiinua mikono itakatayo, pasipo kukasirika na kuchokoza. Vivyo hivyo nataka, penye kuomba wanawake wavae mavazi yafaayo wakijipamba, kama iwapasavyo wenye soni waonyekao; mapambo yao yasiwe misuko ya nywele wala dhahabu wala ushanga wala nguo zilizo za mali nyingi. Ila mapambo yao yawe matendo mema yawapasayo wanawake wanaoungama kuwa wake Mungu! Mwanamke sharti ajifunze kutulia na kutii sana! Lakini simpi mwanamke ruhusa kufundisha, wala kumtawala mumewe, ila akae na kutulia. Kwani Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, halafu Ewa. Naye Adamu siye aliyedanganyika, ila mwanamke ndiye aliyedanganyika, akatangulia kukosa. Lakini ataokoka kwa kuzaa watoto, hao wakiwa wenye kumtegemea Mungu na wenye kupendana na wenye kutakaswa mioyo na wenye kuonyeka. Neno hili ni la kweli: Mtu akitaka kazi ya ukaguzi anataka kazi nzuri. Mkaguzi sharti awe mtu asiye na neno la kimkanya, mwenye mke mmoja, asiyekunywa kileo, mwerevu wa kweli, mwema, mpenda wageni, ajuaye kufundisha. Asikae na wanywaji, asiwe mgomvi, ila awe mpole, pasipo matata na pasipo choyo; ajue kuiangalia vizuri nyumba yake mwenyewe, hata watoto wake wawe wenye kutii na kuwapa watu wote macheo. Maana mtu asiyeweza kuiangalia nyumba yake mwenyewe atawezaje kuwatunza wateule wa Mungu? Mtu aliye Mkristo mpya asiwe mkaguzi, asijitutume, akaja kuanguka katika hukumu ya Msengenyaji. Nao walioko nje sharti wamshuhudie kuwa mwema, asije kusingiziwa mabaya, akanaswa na tanzi la Msengenyaji. Vivyo hivyo nao watumikiaji wa wateule wawe wenye macheo, wasiosema kuwili, wasio walewi, wasiofuata machumo mabaya, ila waliangalie lile fumbo walitegemealo katika mioyo itakatayo kwa kujua tu yaliyo mema. Hao kwanza wajaribiwe! Ikijulikana, ya kuwa haliko neno la kuwakamia, basi, wawekwe kuwa watumikiaji. Vivyo hivyo nao wake zao wawe wenye macheo wasiosengenya, wasiokunywa kileo, walio waelekevu katika mambo yote! Watumikiaji sharti wawe kila mtu mume wa mke mmoja, wenye kuwaangalia vizuri watoto wao na nyumba zao wenyewe. Kwani waliotumika vizuri hujipatia fungu zuri, tena kwa hivyo, wanavyomtegemea Kristo Yesu, huona furaha nyingi kwa kumtangaza. Nakuandikia haya, ijapo nangojea, bado kidogo nifike kwako. Lakini kama nakawia, ujue mwenendo unaopasa katika nyumba ya Mungu! Hiyo nyumba ndio wateule wake Mungu aliye Mwenye uzima; nao ndio nguzo na msingi wa kuyashikiza yaliyo ya kweli. Kweli fumbo lililo kuu ni lile la kumcha Mungu: Mungu alitokea waziwazi mwilini, akapata wongofu kwa kuwa mwenye Roho, akaonekana penye malaika, akatangazwa kwa wamizimu, akategemewa ulimwenguni, akapazwa mbinguni kwenye utukufu. Lakini Roho anasema waziwazi: Siku za mwisho watakuwako watakaoacha kumtegemea Mungu, wakifuata rohoroho za upotevu na mafundisho ya mapepo: ndio watu waliodanganywa nao wanaojitendekeza kwa kusema uwongo na kwa kuficha, ya kuwa wenyewe wamechomwa moto mioyoni kwa kufanya hivyo. Ndio wanaokataza watu kuoa, tena hutangaza miiko ya vyakula, Mungu alivyoviumba, wavile na kushukuru, wakiwa wenye kumtegemea na kuyatambua yaliyo ya kweli. *Kwani kila kilichoumbwa na Mungu ni kizuri, wala hakuna chenye mwiko kinacholiwa, watu wakimshukuru. Kwani kinatakaswa kwa neno lake Mungu, watu wanapokiombea. Ukiwafundisha ndugu mambo hayo utakuwa mtumishi mzuri wa Kristo Yesu, nawe utajilisha maneno, tuyategemeayo, tunayoyafundisha kwamba: Ni mazuri; ni hayo, uliyoyafuata nawe. Lakini yale masimulio yasiyo na maana, yapendezayo wazee wa kike tu, yakatae! Jizoeze kumcha Mungu! Kwani mazoezo ya mwili hufalia mambo machache tu; lakini kumcha Mungu hufalia mambo yote, tena kunacho kiago cha uzima wa sasa na cha ule utakaokuwapo. Neno hili ni la kweli, nalo linapasa kushikwa na watu wote. Kwani kwa sababu hii twasumbuka tukigombezwa, ya kuwa tumemngojea Mungu Mwenye uzima aliye mwokozi wa watu wote, kwanza wao wamtegemeao. Mambo haya uyaagize na kuyafundisha!* Mtu asikubeze kwamba: U kijana bado! Ila wenye kumtegemea Mungu uwe kielezo chao cha kujifundishia kusema na kuendelea na kupendana na kumtegemea Mungu na kujitakasa. Mpaka nitakapofika, ufulize kuwasomea na kuwaonya na kuwafundisha! Usiache kuyatunza yale mema, uliyogawiwa kwa kufumbuliwa kwanza, kisha ukayapata kwa kubandikiwa mikono ya wazee. Mambo hayo uyatunze, ushikamane nayo, wote wapate kuona, unavyoendelea! Jiangalie mwenyewe, uyaangalie nayo, unayoyafundisha, ujikaze yayo hayo! Kwani ukiyafanya hayo utajiokoa mwenyewe, hata wanaokusikia. Aliye mzee usimkaripie, ila umbembeleze, kama ni baba yako! Walio waume wazima useme nao, kama ni ndugu zako! Wanawake wazee nao uwabembeleze, kama ni mama zako! Walio wake wazima useme nao na kuyaangalia yote yenye soni, kama ni dada zako! Wanawake wajane walio wajane kweli uwaheshimu! Lakini mwanamke mjane akiwa na watoto au wajukuu, basi, hao wajifunze kwanza kuwaheshimu walio nao nyumbani mwao wenyewe, wakiwalipa wamama na wabibi mema, walioyapata kwao! Kwani hivi vinapendezeka mbele ya Mungu. Lakini aliye mjane wa kweli ni yule aliyeachwa peke yake tu; yeye humngojea Mungu akifuliza kumwomba Mungu na kuwaombea wengine usiku na mchana. Lakini anayezifuata tamaa zake huyo amekwisha kufa akingali yupo bado. Mambo haya uyaagize, watu wasione neno la kuwaonya! Lakini mtu asipowatunza walio ndugu zake, kupita wengine wale waliomo nyumbani mwake, basi, huyo amekwisha kumkana, aliyemtegemea, naye ni mwovu kuliko wale wasiomtegemea Mungu. Mwanamke mjane apaswaye na kuandikiwa ujane ni yule aliyemaliza miaka 60, aliyekuwa mke wa mume mmoja; nayo matendo yake sharti yajulikane kuwa mazuri, kama kukuza watoto au kupenda wageni au kuosha watakatifu miguu au kusaidia wenye maumivu au kufuata matendo mema yawayo yote. Lakini wajane, wasiomaliza bado ile miaka, uwakatae! Kwani hao wangawa wamtumikia Kristo, watakapoingiwa na tamaa ya mume, wanataka kuolewa, ijapo wajiumbue kwamba: Hivyo, walivyomtegemea Mungu kwanza, wamevitangua. Vilevile hujizoeza kuwa wavivu na kutangatanga nyumba kwa nyumba. Nao si wavivu tu, ila wanao upuzi mwingi, hunyatia wengine, husema yasiyopasa. Kwa hiyo nataka, wasio wazee waolewe, wazae watoto, wayaangalie mambo ya nyumbani mwao, mpingani wasimsengenyeshe, kwani hivyo wako waliogeuka wakimfuata Satani. Lakini mwanamke mwenye kumtegemea Mungu akiwa na wajane mwake, na awatunze, wateule wasilemewe, wapate kuwatunza walio wajane kweli. Wazee wanaosimamia vizuri sharti wapewe heshima mara mbili, kupita wengine ni wale wanaojisumbua kulitumikia lile Neno kwa kulifundisha. Kwani Maandiko yasema: Ng'ombe mwenye kupura ngano usimfunge kinywa! Na tena: Mtenda kazi hupaswa na kupewa mshahara wake. Mzee akisutwa, ukatae, wasipokuwapo mashahidi wawili au watatu! Wakosao uwaonye mbele yao wote, wale wengine nao wapate kuogopa! Namtaja Mungu na Kristo Yesu nao malaika waliochaguliwa kuwa mashahidi nikikuagiza sasa, uyashike maneno haya, nalo utakalolifanya lo lote, ulifanye pasipo kuchukizwa wala pasipo kupendezwa na mtu! Usimbandikie mtu mikono upesi! Wala usijitie katika makosa ya wengine! Jiangalie, uwe mng'avu! Usifulize kunywa maji tu, ila utumie mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo lako, likipatwa na manyonge mara kwa mara! Watu wengine makosa yao yako waziwazi, huwaongoza na kuwapeleka penye hukumu; lakini wengine makosa yao hutokea nyuma yao. Vivyo hivyo nayo matendo mazuri mengine yako waziwazi; nayo yasiyo waziwazi hayafichiki. Wote walio katika mafungo ya utumwa sharti wawape mabwana zao heshima zote, Jina la Mungu nao ufundisho wetu usifyozwe! Lakini walio wa mabwana wenye kumtegemea Mungu wasiwabeze, kwa kwamba ni ndugu, ila wawatumikie kupita wengine, kwa sababu nao wamemtegemea Mungu! Inafaa, wapendwe, maana nao hutaka kuwafanyizia kazi njema. Mtu akifundisha mengine, asiposhikamana na maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo yatupayo uzima wala na ufundisho upasao wenye kumcha Mungu, basi, mtu huyo ametutumka, hana, akijuacho, kilema chake ni mashindano na mabishano ya kujisemea tu. Hayo ndiyo yanayoleta wivu na ugomvi na matusi na masingizio mabaya na machukivu yasiyokoma. Hao huwa kama wenye wazimu waepukao kabisa kwenye kweli, ndio wanaodhani kwamba: Kumcha Mungu ni chumo. Walio hivyo jitenge nao! *Kweli kumcha Mungu ni chumo kubwa, kukiwa pamoja na kutoshewa nayo, tuliyo nayo. Kwani hakuna, tulichokileta humu ulimwenguni, wala hakuna, tuwezacho kutoka nacho tena. Lakini tukiwa na vyakula na vya kuvaa tuseme: Vinatutoshea! Lakini wanaotaka kupata mali nyingi huanguka penye majaribu na matanzi na tamaa nyingi zisizo na maana, ziponzazo watu na kuwatumbukiza maangamizoni, wanapopata kuoza tu. Kwani choyo ni shina la maovu yote. Wengine walikifuata, wakapotelewa, wasiweze kumtegemea Mungu tena, wakajipatia maumivu mengi. Lakini wewe uliye mtu wa Mungu hayo yakimbie! Ukimbilie wongofu na kumcha Mungu na kumtegemea na kupendana na kuvumilia na kujinyenyekeza! Vipige vile vita vizuri vya kumtegemea Mungu! Ishike njia ya uzima wa kale na kale, ulioitiwa, ukaungama ungamo zuri mbele ya mashahidi wengi.* Nakuagiza mbele yake Mungu anayevipa vyote uzima na mbele ya Kristo Yesu aliyelishuhudia ungamo lake zuri mbele ya Pontio Pilato, uyalinde uliyoagizwa, yasiwe na doadoa wala kilema, mpaka bwana wetu Yesu Kristo atakapotokea; naye atakayemtokeza kwetu, siku zake zitakapotimia, ni yule anayeshangiliwa kuwa Mwenyezi peke yake, yule mwenye kutawala wafalme na mabwana. Ni yeye peke yake asiyekufa, hukaa mwangani, msimofikiwa na mtu; hakuna mtu aliyemwona, wala hakuna awezaye kumtazama. Yeye aheshimiwe, kwa sababu nguvu ni zake kale na kale! Amin. Walio wenye mali nyingi humu ulimwenguni waagize, wasijikweze, wala wasizitumainie mali, maana hutoweka upesi; ila sharti wamtumainie Mungu anayetupatia yote na kuyafurikisha, tushibe vema. Waagize, wafanye mwenendo mwema wakifuliza kufanya kazi nzuri, wakigawia wengine mema yao kwa kuwa bia moja nao. Hivyo ndivyo, watakavyojiwekea malimbiko yatakayokuwa msingi mzuri, siku zitakapotimia za kuupata uzima ulio wa kweli. Timoteo, yalinde, uliyopewa ya kuyaweka! Yakatae yale mapuzi yaliyo ya bure tu nayo yale mabishano ya utambuzi ulio wa uwongo tu! Maana wengine walioufuata wamepotelewa na njia ya kumtegemea Mungu. Upole uwakalie ninyi! Amin. Mimi Paulo niliye mtume wa Kristo Yesu kwa hayo, Mungu ayatakayo, nikitangaze kiagio cha uzima uliomo mwake Kristo Yesu, nakuandikia barua, wewe Timoteo, mwanangu mpendwa. Upole ukukalie na wema na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu, Bwana wetu! Namshukuru Mungu, ninayemtambikia tangu siku za baba zangu kwa moyo utakatao kwa kujua mema tu. Nakukumbuka pasipo kukoma nikiomba usiku na mchana. Nami nikiyakumbuka machozi yako, ninatunukia kukuona wewe, furaha zinifurikie. Maana nakukumbuka moyoni, unavyomtegemea Mungu pasipo ujanja; kwanza bibi yako Loi alikukalia kumtegemea Mungu vivyo hivyo, kisha mama yako Eunike naye, lakini moyo wangu unajua, ya kuwa hata wewe unako. Kwa sababu hii nakukumbusha, uyafuate yale mema yaliyomo mwako, uliyogawiwa hapo, nilipokubandikia mikono. Kwani Mungu hakutupa Roho ya kutuogopesha, ila ya kututia nguvu na upendo tuonyeke. Basi, usiingiwe na soni ya kumshuhudia Bwana wetu, hata mimi niliyefungwa kwa ajili yake! Ila ukiumizwa vibaya kwa ajili ya Utume mwema vumilia pamoja nami kwa nguvu za Mungu! Maana ndiye aliyetuokoa, ndiye aliyetuitia kuwa watakatifu; naye hakutuitia kwa hivyo, matendo yetu yalivyo, ila kwa hiyovyo, alivyotaka mwenyewe toka kale kutugawia yale mema yaliyomo mwake Kristo Yesu; ni yayo hayo, tuliyolimbikiwa mbele ya mwanzo wa siku za kale. Lakini siku za sasa yametufunikia hapo, mwokozi wetu Kristo Yesu alipotokea; ndiye aliyezitangua nguvu za kifo, kisha akatokeza mwangani uzima usioangamika, kama tulivyoambiwa na Utume mwema; nami nikawekwa kuutangaza na kuutumikia na kuufundisha. Kwa sababu yake nateseka hivyo, lakini sivionei soni, kwani namjua, nimtegemeaye. Tena ninalo shikizo hili la kwamba: Yuko na nguvu ya kulilinda limbiko langu, mpaka siku ile itakapotimia. Uliyoyasikia kwangu mimi, shikamana nayo! Kwani ni kielezo cha kujifundishia yale maneno yatupayo uzima, tukimtegemea Kristo Yesu na kumpenda! Hilo limbiko zuri sharti ulilinde kwa nguvu za Roho takatifu ikaayo ndani yetu sisi! Neno lile nalijua, ya kuwa wote walioko Asia wameniacha; miongoni mwao wamo Figelo na Hermogene. Bwana awahurumie wao wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa kuwa amenipoza moyo mara nyingi; hakuwa na soni ya mafungo yangu, ila alipofika Roma akajipingia kunitafuta, mpaka akiniona. Bwana ampe kuona huruma kwake Bwana siku ile! Nayo yote, aliyonitimikia huko Efeso, wewe umeyatambua kuliko mimi. Basi wewe mwanangu, ujipatie nguvu, tunazogawiwa tukiwa wake Kristo Yesu! Nayo mambo, uliyoyasikia kwangu mbele yao wengi waliosikiliza, hayo uwalimbikishe watu welekevu watakaoweza kufundisha hata wengine. Vumilia ukiteswa vibaya pamoja nami, kama inavyompasa askari mzuri wa Kristo Yesu! Hakuna askari wa kwenda vitani anayejitia katika machumo ya pamba, ampendeze yule mwenye vita. Lakini mtu angawa anashindana, hafungwi kilemba asiposhinda kikweli. Mkulima ajisumbuaye na kulima imempasa kuyalimbua matunda. Itambue maana yao, nisemayo! Kwani Bwana atakupa utambuzi katika mambo yote. *Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa katika wafu, aliyezaliwa katika uzao wa Dawidi, kama nilivyoutangaza Utume mwema. Kwa ajili yake nateseka vibaya, mpaka nikifungwa kama mwenye maovu, lakini Neno la Mungu halifungiki. Kwa hiyo nayavumilia yote kwa ajili yao waliochaguliwa, kwamba nao waupate wokovu uliomo mwake Kristo Yesu, wafike penye utukufu wa kale na kale. Neno hili ni la kweli: Kama tumekufa pamoja naye; kama twavumilia pamoja naye, tutatawala pamoja naye; kama tutakana kwamba: Hatu wake, naye atatukana sisi; kama hatumtegemei, yeye hufuliza kuwa mwelekevu, kwani hawezi kujikana mwenyewe.* Wakumbushe mambo hayo na kuwaonya mbele yake Mungu, wasibishane! Maana haifai kitu, huwapotoa tu wenye kusikiliza. Jipingie kujitokeza kwa Mungu kuwa mfanya kazi aliye wa kweli, asiyefanya mambo yenye soni, anayelilinganisha vema neno la kweli, atakalogawia watu! Lakini penye upuzi wa bure usio na maana uepuke! Kwani wako watakaoendesha mambo ya kumbeza Mungu, nalo neno lao litaambukiza kama ukoma; miongoni mwao hao wamo Himeneo na Fileto waliopotelewa nayo yaliyo ya kweli wakisema: Ufufuko umekwisha kuwapo. Ndivyo, walivyokosesha hata wengine, wasimtegemee Bwana tena. Lakini msingi, Mungu aliouweka, uko, umeshupaa vivyo hivyo, hujulikana kwa muhuri yake, ni hii: Bwana huwatambua walio wake! Tena: Kila mwenye kulitambikia Jina la Bwana atenguke penye upotovu! Katika nyumba kubwa hamna vyombo vya dhahabu au vya fedha tu, ila vimo hata vyombo vya miti na vya udongo; navyo vingine ni vya mapambo, vingine ni vya machafu. Mtu akiwaepuka wale watu, asijichafue, atakuwa chombo cha pambo kilichotakaswa, naye mwenye nyumba atakitumia, maana kimefalia kazi zote zilizo njema. Tamaa za ujana zikimbie, ukimbilie kupata wongofu na kumtegemea Mungu na kupendana na kupatana nao wote wanaomtambikia Bwana kwa mioyo itakatayo! Lakini mabishano ya upuzi wa watu wasioonyeka yakatae! Jua, ya kuwa huleta magombano tu! Lakini aliye mtumwa wa Bwana haimpasi kugombana, sharti awaendee wote kwa unyenyekevu akijua kuwafundisha, akivumilia wenye uovu. Akiwa mpole hivyo ataweza kuwaonya wapingani nao, kama Mungu anawajutisha, wayatambue yalio ya kweli; kisha watalevuka, wajinasue matanzini mwa Msengenyaji, ambaye walinaswa naye, wamfanyizie, ayatakayo yeye. Lakini yatambue haya: siku za mwisho patakuwa na siku ngumu. Kwani watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye choyo, wenye kujitutumua na kujikweza, wenye matusi, wasiwatii wazazi, wasishukuru, wasimche Mungu, wasiwapende wenzao, wasitake kupatanishwa na mtu kwa kupenda usengenyaji, wasijikataze lo lote, wasionyeke, wasipende mema yo yote, ila watakuwa wachongezi na wakorofi na wenye majivuno; kuzifuata tamaa za miili watakupenda kuliko kumfuata Mungu; watajitendekeza kuwa wenye kumcha Mungu, lakini nguvu yake huipingia. Walio hivyo uwaepuke! Kwani wenzao ndio wale wanaonyemelea nyumbani mwa watu, watongoze wanawake wanyonge waliolemewa na makosa, wakiongozwa na tamaa nyingi; hao hufundishwa toka kale, lakini hapana, watakapoweza kuufikia utambuzi wa kweli. Kama Yane na Yambure waliombisha Mose, ndivyo, hata hao wanavyoyabisha yalio ya kweli; hufanana nao wenye wazimu, wakajulika kuwa wenye kumtegemea Mungu bure tu. Lakini hawataendelea sana, kwani upumbavu wao utawatokea wote waziwazi, kama hata upumbavu wao wale ulivyojulika. Lakini wewe umeufuata ufundisho wangu na mwenendo wangu na mawazo yangu na njia yangu ya kumtegemea Mungu na utulivu wangu na upendo wangu na uvumilivu wangu, hata mafukuzo na mateso yangu, niliyoyapata huko Antiokia na Ikonio na Listra. Nami niliyavumilia hayo mafukuzo yote, naye Bwana akaniokoa katika yote. Nao wote wanaotaka kuishi na kumcha Mungu kwa kuwa wake Kristo Yesu sharti wapate mafukuzo. Lakini watu walio wabaya na wadanganyi wataendelea, wajifikishe palipo pabaya; hupoteza watu, tena hupotezwa wenyewe. *Lakini wewe ukae na kuyashika yale, uliyofundishwa, uliyoyatambua kwamba: Ndiyo ya kweli, maana unajua, waliokufundisha walivyo. Tena kwa sababu umeyajua Maandiko matakatifu tangu utoto wako, haya yanaweza kukuerevusha, uokoke kwa kumtegemea Kristo Yesu. Kwani kila neno la Maandiko, mtu aliloambiwa na Mungu, linafaa, litufundishe, lituonyeshe ubaya wetu, liitulize mioyo yetu, lituonye, tupate wongofu; ndivyo, anavyotengenezewa mtu wa Kimungu ajikazaye kufanya kazi njema zo zote.* Namtaja Mungu naye Kristo Yesu atakayewahukumu wanaoishi hata waliokufa, awe shahidi, nikikuagiza haya: Kwa hivyo, atakavyotokea, ausimike ufalme wake, litangaze Neno! Fuliza hivyo, pafaapo napo pasipofaa! Waonyeshe ubaya wao, wagombeze, wakanye ukiwaendea kna uvumilivu wote pamoja na kuwafundisha! Kwani siku zinakuja, watakapoukataa ufundisho utupao uzima, ila kwa hivyo, watakavyozifuata tamaa zao wenyewe, watajitafutia wafunzi wengi wa kuwafundisha yapendezayo masikioni pao. Nao watajigeuza, wasiyasikilize tena yaliyo ya kweli, wayageukie yalio masimulio tu. *Lakini wewe levuka katika mambo yote! Vumilia ukiteswa vibaya! Fanya kazi ya mpiga mbiu njema! Utimize utumishi wako! Kwani mimi pamenifikia, niwe ng'ombe ya tambiko, nayo siku yangu ya kufunguliwa kutoka ulimwenguni iko karibu. Nimelishindania shindano zuri, nimeimaliza mbio, sikuacha kumtegemea Bwana. Lisaalo ni kufungwa kilemba kipasacho waongofu, nilichowekewa nami Siku ile nitakipata kwake Bwana aliye mhukumu mwenye kweli; lakini si mimi tu atakayekipata, ila nao wote waliokuwa wamempenda, atokee waziwazi.* Jikaze, ufike kwangu upesi! Kwani Dema ameniacha, kwa kuyapenda mambo ya dunia hii akaenda zake Tesalonike. Kreske amekwenda zake Galatia, Tito amekwenda zake Dalmatia. Luka peke yake yuko pamoja nami. Mchukue Marko, uje pamoja naye! Kwani hunitumikia vizuri sana. Tikiko nalimtuma Efeso. Utakapokuja ulete na lile joho gumu, nililoliacha huko Tiroa kwa Karpo! Vilete hata vile vitabu! Nivitakavyo sana, ni vile vya ngozi. Alekisandro, yule mfua shaba amenifanyia maovu mengi; Bwana atamlipa, kama matendo yake yalivyo. Hata wewe ujilinde kwa ajili ya mtu huyo, kwani ameyapinga sana maneno yetu. Nilipojikania mara ya kwanza, hakuwapo hata mmoja aliyesimama upande wangu, wote waliniacha. Wasihesabiwe jambo hili! Lakini Bwana alisimama upande wangu, akanipa nguvu, maana alitaka, ile mbiu itimizwe nami mimi, wamizimu wote wapate kuisikia. Nami nikaokolewa kinywani mwa simba. Naye Bwana akaniokoa katika mambo mabaya yo yote, nipone, niingie katika ufalme wake wa mbinguni. Yeye atukuzwe siku zote kale na kale! Amin. Nisalimie Puriska na Akila walio wa nyumbani mwa Onesifiro! Erasto alisalia Korinto, Tirofimo nalimwacha mgonjwa Mileto Jikaze, ufike, siku za kipupwe zitakapokuwa hazijatimia! Wanakusalimu Eubulo na Pude na Lino na Klaudia na ndugu wote. Bwana awe na roho yako! Upole uwakalie ninyi! Amin. Mimi Paulo ni mtumwa wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo kwamba: Waliochaguliwa na Mungu wapate kumtegemea na kuyatambua yaliyo ya kweli; ndiyo yaliyotufundisha kumcha Mungu na kuungojea uzima wa kale na kale. Huu ndio wa kiagio, Mungu asiyesema uwongo alichokiweka siku za kale mwenyewe, lakini siku zake zilipotimia, akalifufua Neno lake akiitangaza mbiu, niliyopewa nami kuipiga, kama nilivyoagizwa na mwokozi wetu Mungu. Nakuandikia wewe, Tito, maana u mwanangu wa kweli kwa hivyo, tulivyo mmoja kwa kumtegemea Mungu. Upole ukukalie na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba na kwa mwokozi wetu Kristo Yesu! Kwa sababu hii nilikuacha katika Kreta, uyatengeneze yaliyosalia, uiweekee miji yote wazee, kama nilivyokuagiza: akiwa mtu asiye na neno la kumkamia, aliye mume wa mke mmoja, tena mwenye watoto waelekevu wasiosingiziwa kuwa waasherati wala wabezi. Kwani mkaguzi imempasa kuwa mtu asiye na neno la kumkamia, maana humtunzia Mungu walio wake. Asiwe mwenye kujipendeza wala mwenye makali wala mywaji wala mgomvi wala mwenye machumo mabaya! Ila sharti awe mpenda wageni na mpenda mema na mwerevu wa kweli na mwongofu na mcha Mungu na mwenye kujikataza mabaya! Sharti ashikamane na kulitegemea Neno, tulilofundishwa, maana ajue kuituliza mioyo yao wale, atakaowafundisha njia ya uzima, tena ajue kuwashinda hata wabishi. Kwani kuna wengi wasiotii, walio wapuzi na wapotevu. Wapitao wengine ndio wale waliotahiriwa; hupaswa na kufumbwa vinywa, kwani hufudikiza nyumba nzima wakifundisha yasiyopasa, wapate mali; hili ndilo chumo lao baya. Mfumbuaji wa kwao aliyekuwa mwenzao wenyewe alisema: Wakreta ndio waongo kabisa, ni nyama waovu, ni matumbo mavivu; ushuhuda huu ni wa kweli. Kwa sababu hii uwagombeze kwa ukali, wapate kupona na kumtegemea Mungu, wasiyashike masimulio ya Kiyuda, wala maagizo ya watu waliogeuka na kuyaacha yalio ya kweli. Wenye kutakata mioyo, vyote huwatakatia; lakini wenye mioyo michafu wasiomtegemea Mungu hakuna kiwatakiacho, maana hata mawazo yao ni machafu, mioyo isijue tena yatakatayo. Huungama kwamba: Tumemjua Mungu, lakini kwa matendo yao hakuna kuwa wake. Kwani hutapisha, kwa kuwa hawatii, hawafai kabisa kufanya kazi yo yote iliyo njema. Lakini wewe sema yapatanayo na ufundisho utupao uzima! Waume wazee sharti wawe watu wasiokunywa kileo, wapewe macheo, wawe werevu wa kweli, wajipatie uzima kwa kumtegemea Mungu na kwa kupendana na kwa kuvumilia kwao! Vivyo hivyo wanawake wazee nao sharti wafanye mwenendo uwapasao walio watakatifu! Wasisengenye wala wasiwe watumwa wa unywaji wa pombe nyingi, ila wenye kufundisha wengine yaliyo mazuri, wapate kuwaerevusha wanawake walio vijana bado, wawapende waume na watoto wao! Hivyo nao wake vijana watakuwa werevu wa kweli, wang'avu, wenye kutengeneza nyumba zao vizuri, wenye wema na wenye kuwatii waume wao, Neno la Mungu lisibezwe. Lakini vilevile waambie vijana waume na kuwakanya, waerevuke kweli! Katika mambo yote ujiweke mwenyewe kuwawia kielezo cha kujifundishia matendo mazuri! Wafundishe kujiangalia miili, waipe macheo yaipasayo! Litangaze Neno litupalo uzima lisilobishika, mpingani aingiwe na soni, asiweze kusema neno ovu lo lote la kutusuta! Walio watumwa waambie, wawatii mabwana zao, wawapendeze katika mambo yote, wasiwe wabishi, wasiibe ila wajionyeshe kuwa wenye welekevu na wema wote, matendo yao yote yawe mapambo ya ufundisho wa mwokozi na Mungu wetu! *Kwani mema yake Mungu, ayagawiayo watu wote ya kuwaokoa, yametokea waziwazi, nayo hutuonya, tuuvunje mwenendo wa kimizimu, tusizifuate tamaa za humu ulimwenguni, ila siku hizi za sasa za kuishi duniani tuwe wenye werevu wa kweli na wenye wongofu na wenye kumcha Mungu. Kisha tuchungue, kingojeo chetu cha kutushangiliza kitakavyotimia, utukufu wa Mungu wetu mkuu na wa mwokozi wetu Kristo Yesu utakapotokea. Yeye ndiye aliyejitoa mwenyewe kwa ajili yetu kuwa kole ya kuyalipa mapotovu yote, ajipatie watu wang'avu watakaokuwa wake wenye bidii ya kufanya kazi nzuri.* Hayo yaseme na kuwaonya na kuwashinda wakosaji kwa nguvu zote! Mtu asikubeze Wakumbushe wajinyenyekeze penye wakuu na wenye nguvu, wamtii na kujiweka tayari kufanya kazi njema zo zote! Wasitukane mtu, wala wasichokoze wenyewe, ila wajionyeshe kuwa wenye mambo yapasayo, wawaendee watu wote kwa upole kabisa! Kwani hata sisi kale tulikuwa wapumbavu waliokataa kutii; tulikuwa tumepotea, tukazitumikia tamaa nyingi zilizotupendeza, tukaendelea kuwa wenye maovu na wivu na machukivu ya kuchukiana sisi kwa sisi. *Ndipo, ulipotutokea utu wake mwokozi na Mungu wetu aliyetupenda sisi watu, akatuokoa sisi, lakini si kwa sababu ya matendo ya wongofu, tuliyofanya sisi; ila kwa huruma yake yeye alituponya akituosha maji ya kutuzaa mara ya pili, tukawa watu wapya kwa kupewa Roho takatifu; hii ndiyo aliyotumiminia, ikatifurikia, alipomtuma mwokozi wetu Yesu Kristo. Kwa mema yake yeye, aliyotugawia, tukapata wongofu, tukawekewa nasi urithi wetu penye uzima wa kale na kale, kama tunavyongojea.* Hili neno ni la kweli. Nami nataka, mambo haya uyafundishe kwa nguvu ya kuwashinda, maana wale waliomtegemea Mungu wazitunze kazi zao, ziwe nzuri kuliko za wengine. Haya ni mazuri, nayo huwafalia watu. Lakini mabishano ya upuzi na mambo ya wakale na machokozi na magomvi ya miiko uyaache! Kwani hayafai kitu, ni ya bure tu. Mtu mzushi mwonye mara moja, hata mara mbili! Asipoonyeka, mwepuke! Ujue: Mtu aliye hivyo amekwisha kutengeka, tena hujipatia hukumu mwenyewe kwa kukosa kwake. Nitakapomtuma kwako Artema au Tikiko, jikaze kuja kwangu huku Nikopoli! Kwani ndiko, ninakotaka kuzimaliza siku hizi za kipupwe. Akina Zena aliye mjuzi wa Maonyo na Apolo watume upesi, waende zao; lakini uwatunzie vema, wasikose yawapasayo njiani! Hapo wa kwetu nao wajifunze kufanya kazi zilizo nzuri kuliko za wengine! Ikiwa wanatakwa, na wapatie wengine yatakayowatunza, wasifanane na miti isiyozaa! Wanakusalimu wote walio pamoja nami. Wasalimu wanaotupenda kwa kuwa wenye kumtegemea Mungu! Upole uwakalie ninyi nyote! Amin. Mimi Paulo niliyefungwa kwa ajili yake Kristo Yesu na ndugu yetu Timoteo tunakusalimu wewe, Filemoni, uliye mpendwa wetu na mwenzetu wa kazi. Tunakusalimu na wewe, Apia, uliye dada yetu, na wewe, Arkipo, uliye mwenzetu wa kupiga vita. Tunawasalimu nao wateule wote waliomo nyumbani mwako. Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo! Namtolea Mungu wangu shukrani siku zote nikikukumbuka katika kuomba kwangu. Kwani nimesikia, unavyompenda Bwana Yesu na kumtegemea, hata unavyowapenda watakatifu wote. Nakuombea, hivyo, tulivyo mmoja kwa kumtegemea Mungu, vikupe nguvu ya kutambua kwamba: Mema yote, mlio nayo, sharti mmrudishie Kristo! Kwani twalifurahi sana, mioyo yetu ikatulia kwa ajili ya upendo wako, maana roho za watakatifu umezipatia kituo wewe, ndugu yangu. Kwa hiyo, ijapo Kristo anipe moyo mkuu wa kukuagiza likupasalo, kwa ajili ya ule upendo wako nataka kukubembeleza tu. Tazama mimi Paulo nilivyo! Ni mzee, tena hata sasa mfungwa wake Kristo Yesu. Nakubembeleza kwa ajili ya mtoto wangu, niliyemzaa humu kifungoni mwangu; ndiye Onesimo asiyekufalia kale, lakini sasa anatufalia sana, wewe hata mimi. Nikimrudisha kwako, ni kama nitautuma moyo wangu mwenyewe, ukufikie. Nami nalitaka kumshika, akae kwangu, akufanyizie kazi hii ya kunitumikia humu kifungoni, nilimotiwa kwa ajili ya kuutangaza Utume mwema. Lakini kwa kuwa hujaweza kuitikia, sikutaka kufanya kitu, kusudi wema wako usiwe wa kushurutishwa, ila uwe wa kupendezwa mwenyewe. Kwani labda kwa sababu hii ametengwa nawe siku chache, upate kuwa naye kale na kale. Tena sasa siye kama mtumwa tu, ila apita mtumwa kwa kuwa hata ndugu mpendwa; kweli mimi nampenda, nawe utanipita kwa kumpenda, maana ni wako kwanza kimtu, tena ni wako Kikristo. Basi, kama waniwazia kuwa mwenzio, mpokee yeye kama mimi! Lakini kama kiko chako, alichokipotoa, au kama yuko na deni kwako, hayo nibandikie mimi! Mimi Paulo nimeviandika hivi kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitayalipa. Sitakuambia: U mdeni wangu mimi, deni lako ni moyo wako. Kweli, ndugu yangu, nataka kuona upato kwako, maana u wake Bwana. Upatie moyo wangu kituo kwake Kristo! Nimekuandikia, kwa sababu nimejipa moyo wa kwamba: Utatii, tena najua, ya kuwa utafanya kuyapita yale, niliyoyasema. Kisha nitengenezee chumba cha kufikia! Kwani kingojeo hiki ninacho cha kwamba: Mtanipata tena kwa ajili ya kuomba kwenu. Wanakusalimu akina Epafura aliyefungwa pamoja nami kwa ajili ya Kristo Yesu na Marko na Aristarko na Dema na Luka walio wenzangu wa kazi. Upole wa Bwana Yesu Kristo uzikalie roho zenu! Amin. Kale Mungu alisema na baba zetu vinywani mwa wafumbuaji mara nyingi na kufuata njia. Siku hizi za mwisho amesema na sisi kinywani mwa Mwanawe, aliyemweka kuwa kibwana chao yaliyo yake yote. Yeye ndiye, ambaye aliumba naye hata ulimwengu wote. Huyu hutuangazia utukufu wake, kwani kama Mungu alivyo, ndivyo, naye alivyo; tena yeye huvitunza vyote kwa Neno lake lenye nguvu. Alipokwisha kutupatia osho liyaondoalo makosa, akaketi kuumeni kwa mwenye ukuu mbinguni juu, akapata kuwa mtukufu kuliko malaika kwa hivyo, alivyorithi Jina linalolipita lao. Kwani yuko malaika, Mungu aliyemwambia siku iwayo yote: Wewe ndiwe Mwanangu, siku hii ya leo mimi nimekuzaa? Na tena: Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu? Kwa ajili ya siku, alipotaka kumwingiza mzaliwa wake wa kwanza tena ulimwenguni, anasema: Malaika wote wa Mungu sharti wamwangukie yeye!* Mambo ya malaika anayasema kwamba: Huwatumia malaika zake kuwa upepo nao watumishi wake kuwa mioto iwakayo. Lakini mambo ya mwana anayasema kwamba: Mungu, kiti chako cha kifalme kiko kale na kale pasipo mwisho, nayo fimbo ya ufalme wako ndiyo fimbo inyoshayo mambo ya watu. Wewe ulipenda wongofu, ukachukia upotovu. Kwa hiyo Mungu aliye Mungu wako alikupaka mafuta ya kufurahisha kuliko yale ya wenzio. Tena anasema: Wewe Bwana, mwanzoni uliiweka misingi ya nchi, mbingu nazo ni kazi ya mikono yako wewe. Hizo zitaangamia, lakini wewe unafuliza kuwapo. Kweli, zote zitachakaa kama nguo, nawe utazizinga kama nguo ya kujitandia; zitachujuka kama nguo. Lakini wewe ndiwe yuleyule uliyekuwa, miaka yako haitakoma. Lakini yuko malaika, aliyemwambia po pote: keti kuumeni kwangu, mpaka niwaweke adui zako chini miguuni pako? Hawa wote si roho tu za kutumika zitakazotumwa kuwatumikia wale watakaourithi wokovu? Kwa hiyo imetupasa kujikaza, tushikamane nayo, tuliyoyasikia, tusitengeke penye wokovu! Kwani neno lile lililosemwa na malaika lilikuwa na nguvu; kila aliyepitana nalo naye aliyekataa kulisikia akapata lipizi limpasalo. Je? Sisi tutalikimbia tunapoubeza wokovu ulio mkuu kama huu? Kwani ulianza kutangazwa naye Bwana, kisha ukashupazwa kwetu nao waliousikia. Naye Mungu akaushuhudia na kufanya vielekezo na vioja na vyenye nguvu vingi na kuwagawia watu Roho takatifu kila mtu, kama alivyomtakia. Kwani malaika sio, aliowapa kuutawala ulimwengu utakaokuja, tunaousema. Lakini pako paliposemwa ushuhuda wa kwamba: Mtu ndio nini, umkumbuke? Mwana wa mtu naye, umkague? Ulimpunguza kidogo, asilingane na malaika, ukamvika kilemba chenye utukufu na macheo, yote pia ukayaweka kuwa chini miguuni pake. Basi, hapo, alipoviweka vyote chini yake, hakukisaza hata kimoja, asichokiweka chini yake. Lakini sasa hatujaona bado, ya kuwa vyote vimewekwa chini yake. Lakini kule kwamba: Alipunguzwa kidogo, asilingane na malaika, tunaona, ya kuwa kumetimia kwake Yesu. Kwa hivyo, alivyokufa matesoni, alivikwa kilemba chenye utukufu na macheo, maana aligawiwa na Mungu, awaonjee wote uchungu wa kufa. Kwani ni kwa ajili yake Mungu, vyote vikiwapo, naye ndiye aliyeviumba vyote; kwa hiyo ilimpasa, ile kazi ya kutimilika matesoni ampe yule aliyepeleka wana wengi kwenye utukufu alipowaokoa, apate kuwa kiongozi wao. Kwani mwenye kutakasa nao wenye kutakaswa, wote walitoka kwake yeye mmoja. Kwa sababu hii haoni soni ya kuwaita ndugu akisema: Nitawasimulia ndugu zangu mambo ya Jina lako, nitakuimbia wewe katikati yao walio wateule. Tena anasema: Mimi nitakuwa ninamwegemea yeye. Tena anasema: Tazama mimi niko pamoja na hawa watoto, Mungu alionipa. Kwa sababu wale watoto wanayo miili yenye damu na nyama, vivyo hivyo na yeye alijipa mwili ulio hivyo kama yao; kwani alitaka, kufa kwake kumtangue yule aliyekuwa mwenye nguvu za kufa, maana ndiye yule Msengenyaji. Hivyo alitaka kuwakomboa wote walioshikwa utumwani siku zote za maisha yao, wakiogopa kufa. Kwani aliovitunzia hivyo, sio malaika, ila ndio wao wa uzao wake Aburahamu, aliowatunzia. Kwa hiyo ilimpasa kufanana na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa mtambikaji mkuu aliye mwenye huruma na welekevu machoni pake Mungu, aweze kuwa kole ya kuyalipa makosa ya watu. Kwani kwa hivyo, alivyoteseka na kujaribiwa mwenyewe, anaweza kuwasaidia wanaojaribiwa. Kwa hiyo, ndugu zangu watakatifu, mlioitwa kama sisi na mwito utokao mbinguni, yaelekezeni macho kwake Yesu, tunayemwungama kuwa mtume na mtambikaji mkuu! Naye aliyempa kazi hiyo alimtumikia kwa welekevu, kama Mose alivyotumika katika nyumba yake yote. Lakini huyu amepaswa kutukuzwa kuliko Mose; ni vivyo hivyo kama vya nyumba; mwenye kuijenga hupata cheo kuliko ile nyumba yenyewe, kwani kila nyumba hujengwa na mtu. Lakini anayevitengeneza vyote ndiye Mungu. Naye Mose alitumika kwa welekevu katika nyumba yake yote kama mtumishi; hivyo aliyashuhudia yale yatakayosemwa. Lakini Kristo alitumika kama mwana aliye mwenye nyumba yake. Nayo nyumba yake ni sisi, tunapoikaza mioyo yetu, ichangamke, tena tunapofuliza kujivunia kingojeo chetu mpaka mwisho. Kwa hiyo fanyeni, kama Roho Mtakatifu anavyosema: Leo, mtakapoisikia sauti yake, msiishupaze mioyo yenu, kama hapo, mioyo ilipokuwa yenye uchungu, siku ile ya kujaribiwa kule nyikani. Ndipo, baba zenu waliponijaribu na kunipima, tena walikuwa wameyaona matendo yangu miaka arobaini. Nikachafuliwa moyo nao wa kizazi hicho, nikasema: Siku zote hupotea njia mioyoni mwao; lakini hawakuzitambua njia zangu. Kwa hiyo nilijiapia kwa makali yangu kwamba: Hawataingia kamwe kwenye kituo changu! Tazameni, ndugu, pasiwe mmoja wenu mwenye moyo mbaya usiomtegemea Mungu, ukijitenga kwake yeye aliye Mwenye uzima! Ila mwonyane wenyewe siku kwa siku, pangali pakiitwa leo, kusudi kwenu kusipatikane mwenye moyo mgumu uliodanganywa na ukosaji! Kwani tumekwisha kuwa wenziwe Kristo, tunapokishika kingojeo chetu cha kwanza, kisitupotelee mpaka mwisho. Paliposemwa: Leo, mtakapoisikia sauti yake, msiishupaze mioyo yenu kama hapo, mioyo ilipokuwa yenye uchungu! Hapo walioyasikia na kupata mioyo yenye uchungu walikuwa akina nani? Sio hao wote waliotoka Misri wakiongozwa na Mose? Tena ni akina nani waliochafua moyo wake miaka 40? Sio hao waliokosa, wao waliokufa nyikani, miili yao ikiachwa hapohapo? Tena ni akina nani, aliowaapia kwamba: Hawataingia kamwe kwenye kituo chake, wasipokuwa wale waliokataa kutii? Nasi twaona, ya kuwa hawakuweza kuingia, kwa sababu hawakumtegemea. Kwa kuwa kile kiagio cha kuingia kwenye kituo chake kiko bado, na tuogope, pasionekane hata mmoja wenu ajiwaziaye kwamba: Nimekikosa! Kwani nasi tumepigiwa hiyo mbiu njema kama wale. Lakini wale lile neno, waliloambiwa, halikuwafalia, kwani hawakulitegemea, wajiunge nao walisikiao. Maana sisi tumtegemeao Mungu twaingia kwenye kituo kile, kama alivyosema: Kwa hiyo nilijiapia kwa makali yangu kwamba: Hawataingia kamwe kwenye kituo changu! Nazo kazi zake zilikuwa zimekwisha kufanyika hapo, alipokwisha kuumba ulimwengu, kwani pako mahali, alipoisema maana ya siku ya saba kwamba: Siku ya saba Mungu alizipumzikia kazi zake zote. Napo pale alisema: Hawataingia kamwe kwenye kituo changu! Hivyo vinajulika: wako bado watakaokiingia; lakini wale walioanza kupigiwa mbiu yake njema hawakukiingia, kwani walikataa kutii. Miaka ilipokwisha kupita mingi mno, akaweka tena siku, ni hii ya leo, alipomwambia Dawidi, kama alivyosema kale: Leo, mtakapoisikia sauti yake, msiishupaze mioyo yenu! Kwani kama Yosua angalikuwa amewapeleka kwenye kituo, asingalisema siku nyingine iliyoko nyuma bado. *Kwa hiyo twasema: Liko pumziko, watu wa Mungu walilowekewa bado. Kwani aliyeingia kwenye kituo chake, huyo kuzipumzikia kazi zake yeye, kama Mungu alivyozipumzikia kazi zake mwenyewe. Sasa tujihimize kuingia kwenye kituo kile, pasipatikane mtu atakayeangushwa akiyafuata mafunzo yao walewale waliokataa kutii! Kwani neno la Mungu ni lenye uzima na nguvu, tena ni lenye makali kupita ya upanga wenye makali pande mbili. Nalo hupenya, mpaka litenge moyo na roho, nacho kiini na mifupa. Nalo huyaumbua mapenzi na mawazo yaliyomo moyoni. Hakuna kiumbe kiwezacho kujitowesha mbele yake yeye, ila vyote viko uchi na waziwazi machoni pake yeye, naye ndiye, ambaye tunatangaza Neno lake.* Tunaye mtambikaji mkuu kupita wengine aliyepaa mbinguni, ndiye Yesu, Mwana wake Mungu; kwa hiyo na tuyashike, tunayoyaungama! *Kwani hatuna mtambikaji mkuu asiyeteseka pamoja na sisi kwa ajili ya manyonge yetu. Maana naye alijaribiwa katika mambo yote kama sisi, lakini hakukosa. Kwa hiyo twende, tufike pasipo woga penye kiti chake cha kifalme, tutakapogawiwa huruma na upole, tumwone yeye atakayetusaidia hapo, tutakapomtakia!* Kwani kila mtambikaji mkuu anayechaguliwa katika watu huwekwa kwa ajili ya watu, awafanyizie kazi kwake Mungu akimtolea matoleo na vipaji vya tambiko kwa ajili ya makosa yao. Huyu anaweza kuwavumilia kidogo wasiojua maana, wakipotezwa, kwa sababu hata yeye ni mwenye unyonge. Kwa ajili yake huo hana budi kujipatia mwenyewe kole ya makosa yake yeye vivyo hivyo, kama anavyowapatia watu. Wala hakuna ajipaye mwenyewe cheo hiki, ila huitwa na Mungu, kama naye Haroni alivyoitwa. Vivyo naye Kristo hakujipa utukufu mwenyewe kuwa mtambikaji mkuu, ila ni yeye aliyemwambia: Wewe ndiwe Mwanangu, siku hii ya leo mimi nimekuzaa. Ndivyo anavyosema hata pengine: Wewe u mtambikaji wa kale na kale, kama Melkisedeki alivyokuwa. Naye siku zile allikuwapo mwenye mwili wa kimtu, akamwomba na kumbembeleza yule aliyeweza kumwokoa katika kufa. Alipokaza kumlalamikia na kutoa machozi akasikiwa naye, kwa sababu alimcha Mungu. Naye angawa Mwana, lakini katika kuteswa ndimo, alimojifunzia kutii. Tena hapo, mambo yake yalipotimilika, akawapatia wote wamtiio wokovu wa kale na kale. Kwa hiyo alipewa na Mungu jina la mtambikaji mkuu, kama Melkisedeki alivyokuwa. Hapo tunayo maneno mengi ya kusema, lakini ni magumu ya kuyaeleza vema, nanyi mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwani tukizipima siku, mlizofundishwa, msingekuwa na budi kuwa wafunzi; lakini mwapaswa, mtu aanze tena kuwafundisha, maneno ya Mungu yalivyoanza; maana yawafaliayo ni maziwa, vyakula vigumu sivyo. Kwani kila anayenyonyeshwa maziwa ni mtu asiyejua bado yaongokayo, kwani ni mtoto mchanga. Lakini walio watu wazima hilishwa vyakula vigumu; kwani hao wameizoeza mioyo yao kujua maana, kwa hiyo hupambanua yaliyo mazuri nayo yaliyo maovu. Kwa hiyo na tuyaache mafundisho ya kwanza ya Kristo, tuendelee kuwafundisha yaliyo ya kutimiza! Tusiweke tena msingi na kuwafundisha kwamba: Juteni mkiyaacha matendo yawauayo! Kisha mtegemeeni Mungu! Tuyaache nayo mafundisho ya ubatizo na ya kubandikiwa mikono na ya ufufuko wa wafu na ya hukumu ya kale na kale! Hayo tutayafuata, Mungu atakapotupa ruhusa. Kwani waliokwisha kuangazwa mioyo na kukionja kipaji kitokacho mbinguni na kugawiwa Roho takatifu na kulionja Neno la Mungu lililo zuri na kuzionja nguvu za siku zitakazokuja, basi, walio hivyo wakitengeka, haiwezekani tena kuwapatia upya, wapate kujuta. Kwani hao humwamba msalabani Mwana wa Mungu mara kwa mara pamoja na kumfyoza, huku ndiko kujiangamiza. Kwani nchi, ikiinywa mvua iinyeayo mara nyingi, huzaa maboga yanayowafalia wailimao, ikichipushwa na Mungu. Lakini ikizaa miiba na mibigili haifai tena, ikafikia kuapizwa, nayo mwisho huteketea. Lakini hata tukisema hivyo, wapendwa, kwa ajili yenu ninyi tumejipa moyo wa kwamba: Yale mema yatupayo wokovu mnayo. Kwani Mungu siye mpotovu, hatayasahau matendo ya upendo wenu, mliyoyatumia ya kulikuza Jina lake na kuwatumikia watakatifu toka kale hata sasa. Lakini twataka sana, kila mmoja wenu ajikaze vivyo hivyo, apate kukishika kingojeo chetu chote kizima mpaka mwisho, msipate kuwa wavivu, ila mwaige wale walio wenye kuvirithi viagio kwa hivyo, walivyovitegemea na kuvumilia. Kwani Mungu alipomwekea Aburahamu kiagio aliapa na kujitaja mwenyewe kwa kukosa aliye mkubwa kumpita, amtaje akiapa. Akasema: Nitakubariki kweli, nikupe kuwa watu wengi sana. Naye alipovumilia akaona, kiagio kilivyotimia. Kwani watu wakiapa hutaja aliye mkubwa kuliko wao, nacho kiapo hukomesha kwao mabishano yote na kulitia nguvu lile neno. Naye Mungu alipotaka sana kuwaonyesha wenye kiagio kwamba: Ayatakayo yeye hayatanguki kamwe, akaapa, wapate kutulia. Akataka, hayo mambo mawili yasiyotanguka kamwe - maana haiwezekani, Mungu aseme uwongo - yatupe matulizo yenye nguvu sisi tuliomkimbilia, tupate kukishika kingojeo chetu, tulichowekewa. Hicho tunakishika, kiwe nanga ya moyo isiyokosa nguvu za kutuliza; nacho ndicho kituingizacho namo mle ndani, tulimopingiwa na lile pazia. Humo ndimo, Yesu alimoingia, atufungulie njia, akawa mtambikaji mkuu wa kale na kale, kama Melkisedeki alivyokuwa. Kwani huyo Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu na mtambikaji wa Mungu alioko mbinguni juu. Hapo Aburahamu aliporudi na kutoka katika vita vya wafalme, alimwendea, akampongeza. Naye Aburahamu akamgawia fungu la kumi la mali zote. Maana ya jina lake kwanza ni kwamba: Mfalme wa wongofu; tena ni kwamba: Mfalme wa Salemu, ndio mfalme wa utengemano. Baba yake na mama yake nao wakale wake hawajuliki, wala siku zake za kuishi hazijuliki, zilipoanzia, wala zilipokomea, maana amefananishwa na Mwana wa Mungu, ni mtambikaji wa kale na kale. Lakini tazameni, huyo alivyokuwa, baba yetu mkuu Aburahamu akimpa fungu la kumi la mateka! Kweli nao wana wa Lawi waliopewa utambikaji waliagizwa na Maonyo kuwatoza fungu la kumi wenzao wa ukoo walio ndugu zao, tena ndio waliotoka pamoja nao kiunoni mwa Aburahamu. Lakini yule asiyekuwa wa ukoo wao alimtoza Aburahamu fungu la kumi, akampongeza yule aliyekuwa mwenye kiagio. Lakini hili halibishiki kwamba: Kilicho kidogo hupongezwa nacho kilicho kikubwa. Napo hapo watu walio wenye kufa hutoza fungu la kumi; lakini alilitoza mtu anayeshuhudiwa kwamba: Anaishi. Tena, ikiwezekana kusema hivyo, katika Aburahamu hata Lawi aliye mwenye kutoza fungu la kumi alitozwa naye fungu la kumi. Kwani alikuwa kiunoni mwa babu yake, Melkisedeki alipokutana naye. Kama utambikaji wa Kilawi ungaliyatimiza yote, (kwani hapo, ulipokuwapo, watu walipewa Maonyo), ni kwa sababu gani tena ikisemwa: Sharti painuke mtambikaji mwingine, kama Melkisedeki alivyokuwa, isiposemwa: Kama Haroni alivyokuwa? Kwani utambikaji unapogeuzwa, hapo sharti Maonyo nayo yageuke. Kwani yule aliyesemwa yale maneno alikuwa wa shina jingine, ambalo hakutoka kwake mtu ye yote aliyefanya kazi ya utambikaji. Kwani hujulikana: Bwana wetu alitoka katika shina la Yuda, nalo shina hilo Mose hakuliambia hata neno moja la utambikaji. Tena huelekea kabisa: Pakiinuka mtambikaji mwingine anayefanana na Melkisedeki, yeye utambikaji wake haukutoka kwenye Maonyo yaagizayo mambo ya kimtu, ila umetoka kwenye nguvu ya uzima usiolegezeka. Kwani unashuhudiwa kwamba: Wewe u mtambikaji wa kale na kale, kama Melkisedeki alivyokuwa. Hivyo lile agizo la kale linatanguka, kwa sababu lilikuwa nyonge, tena halikufaa; kwani hakuna lililotimizwa na Maonyo. Lakini mahali pake paliingizwa kingojeo kilicho kikuu kuyapita Maonyo, maana kinatufikisha kwake Mungu. Tena hivi havikufanyika pasipo kiapo: kwani wale wengine waliupata utambikaji pasipo kiapo, lakini huyu aliupata, yeye Mungu akiapa na kujitaja alipomwambia: Bwana aliapa, naye hatajuta: Wewe u mtambikaji wa kale na kale. Hivyo Yesu ni mtimizaji wa agano lililo kuu kulipita lile. Nao wale ni wengi waliokuwa watambikaji, kwa sababu kufa kuliwazuia, wasikae. Lakini huyu anao utambikaji usiopokezanwa, kwa sababu anakaa kale na kale. Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kale na kale wanaomjia Mungu na kumfuata yeye; kwani yeye anaishi siku zote, apate kuwaombea. Kwani mtambikaji mkuu, ambaye tunapaswa naye, ni yule mcha Mungu, asiye mwovu, asiye mwenye madoa, aliyetengeka na wakosaji, alioko juu kuliko mbingu. Hapaswi kama wale watambikaji wakuu, kila siku kwanza kujipatia yeye kole ya makosa yake mwenyewe, kisha kuwapatia watu nao kole ya makosa yao. Kwani huyu amevifanya hivyo mara moja hapo alipojitoa mwenyewe kuwa kole. Kwani Maonyo huweka watu wenye unyonge kuwa watambikaji wakuu. Lakini neno la kiapo kilichoyafuata Maonyo nyuma linamweka Mwana kuwa mtambikaji mtimilifu wa kale na kale. Neno lililo kuu katika hayo, tuliyoyasema, ni hili: Tunaye mtambikaji mkuu aliyeketi mbinguni kuumeni kwa kiti cha kifalme chenye ukuu. Naye ni mtunzaji wa Patakatifu na wa Hema lile la kweli, Bwana alilolisimamisha, siye mtu aliyelisimamisha. Kwani kila mtambikaji huwekwa kupeleka matoleo na vipaji vya tambiko. Kwa hiyo hata huyu amepaswa kuwa na kitu cha kumpelekea Mungu. Kama angekuwa ulimwenguni, asingekuwa mtambikaji, maana wako wanaompelekea Mungu vipaji, kama walivyoagizwa. Nao huvitumikia vile vilivyo mfano na kivuli cha vile vilivyoko mbinguni. Ndivyo, Mose naye alivyoagizwa alipotaka kulitengeneza lile hema, kwamba: Angalia, uyafanye yote kwa mfano, ulioonyeshwa mlimani! Lakini sasa huyu amepata utumikizi ulioupita, kwani agano, alilotuletea, ni zuri kuliko lile, tena limeunganishwa na maagizo na viagio vilivyo vizuri navyo kuliko vile. Kwani lile la kwanza kama lingalikuwa pasipo masazo, pasingalitafutwa mahali pa kuwekea la pili. Kwani anawakanya na kuwaambia: Bwana anasema: Mtaona, siku zikija, ndivyo asemavyo Bwana; ndipo, nitakapowatimilizia wao wa mlango wa Isiraeli nao wa mlango wa Yuda Agano Jipya! Halitakuwa, kama Agano lile lilivyokuwa, nililolifanya na baba zao siku ile, nilipowashika mikono, niwatoe katika nchi ya Misri; kwani wao wenyewe hawakulishika Agano langu, nami nikawakataa; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani Bwana asema: Agano, nitakalolifanya nao wa mlango wa Isiraeli, siku hizi zitakapokuwa zimepita, ni hili, asema Bwana: Nitawapa Maonyo yangu, yakae katika mawazo yao, tena nitayaandika mioyoni mwao; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Hawatafundishana tena mtu na mwenziwe wala mtu na ndugu yake kwamba: Mtambue Bwana! Kwani wote watanijua, hivyo walivyo wadogo, mpaka wakiwa wakubwa. Kwani nitawahurumia kwa ajili ya mapotovu yao, nisiyakumbuke tena makosa yao. Agano anapoliita Jipya, lile la kwanza amekwisha kulifanya kukuu. Lakini lililo kukuu na chakavu limefikia kutoweka. Nalo Agano la kwanza lilikuwa na maongozi ya kumtambikia Mungu, tena lilikuwa na Patakatifu palipopasa ulimwenguni. Kwani palikuwa pamesimamishwa hema la kuingilia; mwake mlikuwamo taa na meza na mikate aliyowekewa Bwana. Ndipo palipoitwa Patakatifu. Lakini mle ndani mbele ya pazia lililoko katikati mlikuwamo hema lililoitwa Patakatifu Penyewe. Humo mlikuwa na kivukizio cha uvumba cha dhahabu tupu na Sanduku la Agano lililofunikizwa po pote na mabati ya dhahabu; ndani yake mlikuwa na kitungi cha dhahabu chenye Mana na fimbo yake Haroni iliyochipuka na vibao vya Agano. Lakini juu ilikuwa imefunikwa na Makerubi yenye utukufu waliokipatia hicho Kiti cha Upozi kivuli. Hayo yote hatuwezi kuyasema sasa moja moja. Hivi vilipokwisha kutengenezwa hivyo, watambikaji huingia kila siku katika hema la kwanza wakifanya kazi za tambiko. Lakini katika hema la pili humwingia mtambikaji mkuu peke yake kila mwaka mara moja tu, naye hamwingii pasipo damu, anayoipeleka, iwe kole yake yeye na ya makosa ya watu wanaojikosea tu. Hivyo Roho Mtakatifu hueleza kwamba: Njia ya kupaingilia Patakatifu Penyewe haijafunguka siku, hema la kwanza litakapokuwa likingali limesimama bado. Nalo lilikuwa mfano wa kuonyesha, siku hizi za sasa zilivyo: kwani mle watu humpelekea Mungu matoleo na vipaji vya tambiko visivyoweza kumpa mwenye kuvitoa moyo uliotulia wote. Kwani miiko ya kula na ya kunywa nayo maosho mengi ni maongozi ya miili tu, yatufikishe hapo, siku za kuinyosha njia zitakapokutia. *Lakini Kristo alikuja kuwa mtambikaji mkuu wa yale mema yatakayotokea, akapita katika hema lililo kubwa na timilifu kulipita lile lililotengenezwa na mikono ya watu, maana halikufanywa na viumbe vilivyopo nchini. Naye hakupeleka damu za mbuzi na za ndama, ila damu yake mwenyewe, akapaingia nayo Patakatifu Penyewe ile mara moja, akatupatia ukombozi usio na mwisho. Kwani kale damu za mbuzi na za ng'ombe na majivu ya mori aliyechomwa yalinyunyiziwa wenye uchafu, yawatakase, uchafu wa miili uwaondoke; lakini sasa kwa hivyo, Kristo alivyojitoa kwa nguvu ya Roho aliye wa kale na kale kumwia Mungu ng'ombe ya tambiko isiyo na kilema, damu yake itazidi kuing'aza sana mioyo yetu yote, tuyaache matendo yenye kutuua, tupate kumtumikia Mungu aliye mwenye uzima. Kwa sababu hii alikuwa mpatanishi aliyetuletea Agano Jipya kwamba: Walioitwa na waupate urithi wao ulio wa kale na kale, kama walivyoagiwa, kwani kufa kumeoneka kunakokomboa katika makosa yaliyofanyika siku za Agano la kwanza.* Kwani hapo palipo na agano, sharti kwanza mwenye kuliweka afe. Kwani agano hutimizwa na kufa, lakini halina maana kabisa, mwenye kuliweka angali yu hai. Kwa hiyo hata lile la kwanza halikueuliwa pasipo damu. Kwani Mose alipokwisha kuwaambia watu wote kila agizo la maonyo, akachukua damu za ndama na za mbuzi, kisha akachukua na maji na pamba nyekundu na kivumbasi, akakinyunyizia Kitabu chenyewe, kisha nao watu wote, akisema: Hizi ni damu za Agano, Mungu alilowaagizia. Hata hema na vyombo vyote vya kutambikia akavinyunyizia damu vilevile. Nayo Maonyo yaliagiza, vyombo vyote vitakaswe na damudamu, maana pasipo kumwagika damu hakuna ondoleo. Basi, mifano ya vile vilivyoko mbinguni ilipasa kutakaswa hivyo. Lakini vile vya mbinguni vyenyewe vilipaswa na vipaji vya tambiko vilivyo vyenye nguvu kuliko vile. Kwani Kristo hakupaingia Patakatifu palipofanywa na mikono, palipo mfano wa Patakatifu pa kweli, ila aliingia mbinguni kwenyewe, atokee sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu sisi. Lakini hakuingia, ajitoe mara nyingi, kama mtambikaji mkuu anavyopaingia Patakatifu kila mwaka na kupeleka damu isiyo yake. Yeye angalipaswa na kuteswa mara nyingi, kuanzia hapo, ulimwengu ulipoumbwa. Lakini sasa ameonekana mara moja tu, siku zilipotimia, azitangue nguvu za ukosaji na kujitoa kuwa kipaji cha tambiko. Kama inavyowapasa watu, wafe mara moja, kisha wahukumiwe, vivyo naye Kristo ametolewa mara moja, awe kipaji cha tambiko cha kuyaondoa makosa ya watu wengi. Lakini mara ya pili atawatokea pasipo kosa wale wanaomngojea, awaokoe. Maonyo hufanana, kama ni kivuli tu cha yale mema yatakayotokea, wala siyo sura yao yenyewe, ni kufanana tu nayo. Navyo vipaji vya tambiko, walivyovipeleka kila mwaka, ni vivyo hivyo kale na kale, navyo haviwezi kuwapa utimilifu wenye kuvitoa. Je? Hao wenye kutambika wakiisha kutakaswa mara moja, kama wasingejua mioyoni kwamba: Makosa yako, hawangeacha kupeleka vipaji vya tambiko? Lakini hivyo vipaji vya tambiko ndivyo vinavyowakumbusha makosa yao mwaka kwa mwaka, kwani damu za ng'ombe na za mbuzi haziwezi kuondoa makosa. Kwa hiyo anasema anapoingia ulimwenguni: Ng'ombe na vyakula vya tambiko hukuvitaka; lakini umenitengenezea mwili. Ng'ombe za tambiko zinazoteketezwa nzima navyo vipaji vya kulipa makosa hukupendezwa navyo. Ndipo, niliposema: Tazama, ninakuja! Mambo yangu yameandikwa katika kitabu cha kale, niyafanye, uyatakayo wewe, Mungu. Kwanza anasema: Ng'ombe na vyakula vya tambiko, nazo ng'ombe za tambiko zinazoteketezwa nzima, navyo vipaji vya kulipa makosa hukuvitaka, wala hukupendezwa navyo, tena hutolewa, kama vilivyoagizwa. Kisha alisema: Tazama, ninakuja, nifanye uyatakayo wewe. Hivyo analitangua lile la kwanza, apate kulisimamisha lile la pili. Kwa hayo, aliyoyataka, tumetakaswa, kwani mwili wake Yesu Kristo ulitolewa mara moja. Kila mtambikaji husimama siku kwa siku akitambika, navyo vipaji vya tambiko, anavyovitoa mara nyingi, ni vivyo hivyo visivyoweza kabisa kuondoa makosa. Lakini huyu alitoa kipaji kimoja tu cha tambiko kwa ajili ya makosa ya watu, nacho ni cha kale na kale, kisha aliketi kuumeni kwa Mungu. Sasa anangoja tu, adui zake wawekwe chini miguuni pake. Kwani kwa kukitoa kile kipaji chake kimoja cha tambiko amewapa wenye kutakaswa utimilifu ulio wa kale na kale. Naye Roho Mtakatifu anatushuhudia hivyo. Kwani kwanza anasema: Bwana anasema: Agano, nitakalolifanya nao, siku hizi zitakapokuwa zimepita, ni hili: Nitawapa maonyo yangu, yakae mioyoni mwao; tena nitayaandika katika mawazo yao. Sitayakumbuka tena makosa yao na mapotovu yao. Basi, hayo yanapoondolewa, hapo hapana tena kutoa kipaji cha tambiko kwa ajili ya ukosaji. *Ndugu, changamko letu la sasa ni hili la kwamba: Tunayo njia inayotuingiza Patakatifu, ni damu ya Yesu; njia hii ni ya siku hizi, tena inatupa uzima; yeye ameifungua hapo, alipopaingia Patakatifu Penyewe, ni hapo, alipoutoa mwili wake. Kwa hiyo tunaye mtambikaji mkuu wa Nyumba ya Mungu. Basi, na tumwendee kwa mioyo yenye kweli, inayojikaza kumtegemea! Kwa hivyo, tulivyonyunyizwa mioyo, isijue tena ubaya, tena kwa hivyo, miili yetu ilivyooshwa kwa maji yatakatayo, na tufulize kukiungama kingojeo chetu, tusichoke! Kwani yeye aliyetupa kiagio chake ni mwelekevu. Tena tuangaliane, tupate kuhimizana, tupendane kwa kufanya matendo mazuri! Kisha tusiache makutano yetu, kama wengine walivyojizoeza, ila tuonyane! Tena tukaze kuonyana kwa hivyo, tunavyoona: Siku ile inakaribia!* Kwani sisi tuliokwisha kuyatambua yaliyo ya kweli tukikosa tena kwa kuyapenda makosa, hakuna kipaji cha tambiko tena kilichotusalia cha kuondoa makosa, ila kinachotusalia ni woga wa kuingoja hukumu na ukali wa moto utakaowala wabishi. Mtu ayatanguaye Maonyo ya Mose huuawa pasipo kuonewa uchungu, akisutwa na mashahidi wawili au watatu. Tena je? Silo lipizi baya kuliko hilo limpasalo mtu, aliyemponda Mwana wa Mungu na kuiwazia damu ya Agano, aliyotakaswa nayo, kwamba: Haifai kitu? Huko siko kumkorofisha Roho aliyemgawia mema? Kwani twamjua aliyesema: Lipizi ni langu mimi, ni mimi nitakayelipisha. Na tena: Bwana atawaamulia walio ukoo wake. Kunatia woga sana kutumbukia mikononi mwa Mungu aliye Mwenye uzima. *Lakini mzikumbuke siku za kwanza, mlipoangazwa! Hapo mlivumilia mapigano mengi mkiteseka. Siku nyingine mkatolewa wenyewe kutazamwa na watu, mkitukanwa pamoja na kuumizwa, siku nyingine mliwatazama wenzenu, wakifanyiziwa hivyo. Kwani wale waliofungwa mliteseka pamoja nao; nanyi mliponyang'anywa, mliyokuwa nayo, mliitikia na kufurahi, kwani mlitambua, ya kuwa mnacho kilimbiko kiyapitacho yale kuwa kizuri, maana hakichakai. Basi, msikitupe kingojeo chenu! Kwani kitawapatia malipo makubwa. Lakini mnapaswa na uvumilivu, myafanye, Mungu ayatakayo, myapokee yale, mliyoagiwa. Kwani pamesalia padogo penyewe, patokee mwenye kuja, hatakawia. Naye mwongofu wangu atapata uzima kwa kunitegemea. Lakini atakayerudi nyuma hataipendeza roho yangu. Lakini sisi hatu wenye kurudi nyuma, tuangamie, ila wenye kumtegemea, tuziokoe roho zetu.* Kumtegemea Mungu ni kuyatumaini, tunayoyangojea, pasipo kuyaonea mashaka yasiyonekana bado. Kwani wakale walishuhudiwa kuwa wenye kumtegemea hivyo. Kwa kumtegemea Mungu twajua, ya kuwa ulimwengu ulitengenezwa kwa Neno lake Mungu, mtu asiseme: Tunavyoviona kwa macho, vilipata kuwapo kwa nguvu yao vile vinavyoonekana. Kwa kumtegemea Mungu Abeli alimtolea Mungu kipaji cha tambiko kilichokuwa kikubwa kuliko chake Kaini, akashuhudiwa nacho kuwa mwongofu, kwani Mungu alipendezwa na vipaji vyake. Naye angawa amekufa, kwa hiyo anasema bado. Kwa kumtegemea Mungu Henoki alichukuliwa, asione kufa. Naye hakuonekana tena, kwa kuwa Mungu alikuwa amemchukua. Naye alipokuwa hajachukuliwa bado, alikuwa ameshuhudiwa, ya kuwa alimpendeza Mungu. Lakini pasipo kumtegemea haiwezekani kumpendeza Mungu. sharti. Kwani atakayemjia Mungu, amtegemee kwamba: Yupo, nao watakaomtafuta huwalipa. Kwa kumtegemea Mungu Noa alionyeshwa mambo yaliyokuwa hayajaonekana bado, naye kwa hivyo, alivyomcha Mungu, akakitengeneza chombo, awaokoe waliokuwamo nyumbani mwake. Ndivyo, alivyouumba ulimwengu, lakini yeye akaurithi wongofu unaopatikana kwa kumtegemea Mungu. Kwa kumtegemea Mungu Aburahamu alitii alipoitwa, ahame, aende mahali, atakapopewa kuwa urithi wake. Akahama, asijue, aendako. Kwa kumtegemea Mungu akawa mgeni katika nchi, aliyoagiwa, kama siyo yake, akakaa katika mahema pamoja na Isaka na Yakobo waliokuwa wenziwe wenye urithi wa kiagio kilekile. Kwani alikuwa akiutazamia mji wenye misingi iliyotengenezwa na kujengwa na Mungu. Kwa kumtegemea Mungu naye Sara alipewa nguvu ya kupata mimba hapo, alipokwisha kuwa mzee; kwani alimwazia yule aliyemwagia hivyo kuwa mwelekevu. Kwa hiyo wale waliozaliwa na yeye mume mmoja aliyekuwa mwenye mwili uliokwisha kufa walikuwa wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa ufukoni penye bahari usiohesabika. Hao wote walikufa na kumtegemea Mungu: kwa kuwa hawakuyapata, waliyoagiwa, ila waliyaona, yako mbali bado, wakaenda kuyakutia kule, wakaungama: Nchini tu wageni wanaopita tu. Kwani wenye kusema hivyo wanaonekana kuwa wenye kutafuta nchi ya kutua. Nao kama wangaliikumbuka nchi ile, waliyotoka, wangaliweza kurudi. Lakini sasa wanaitaka nchi iliyo nzuri kuliko ile, nayo iko mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni soni ya kuitwa Mungu wao, kwani aliwatengenezea mji. Kwa kumtegemea Mungu Aburahamu alipojaribiwa alimtoa Isaka, awe ng'ombe ya tambiko, yeye aliyekuwa mwana wake wa pekee. Naye alikuwa amevipokea viagio, alivyowekewa kwamba: Wa Isaka ndio watakaoitwa uzao wako. Alidhani, ya kuwa Mungu anaweza kuamsha mtu hata kwenye wafu. Kwa hiyo alimpata tena papo hapo, alipokwisha kumtoa. Kwa kumtegemea Mungu Isaka alimbariki Yakobo na Esau kwa ajili ya mambo, watakayoyaona. Kwa kumtegemea Mungu Yakobo alipokuwa mwenye kufa aliwaombea mema kila mmoja wao wana wa Yosefu, akawaombea na kuinama, akiiegemea ncha ya mkongojo wake. Kwa kumtegemea Mungu Yosefu alipofikisha kufa alikumbuka, ya kuwa wana wa Isiraeli wataitoka ile nchi, akawaagizia mifupa yake. Kwa hiyo, wazazi wake walivyomtegemea Mungu, Mose alipozaliwa alifichwa nao miezi mitatu; kwa sababu walimwona mtoto kuwa mzuri, hawakuliogopa agizo la mfalme. Kwa kumtegemea Mungu Mose alipokuwa mtu mzima alikataa kuitwa mwana wa binti Farao, akapendezwa kufanyiziwa maovu pamoja na watu wa Mungu, akayakataa mazuri yaliyopatikana kwa kukosa, maana huishia upesi. Kwani alifikiri hivyo: kubezwa kwa kuwa wake Kristo ni kilimbiko kikuacho kuliko mali zote za Misri, maana aliyatazamia malipo ya mwisho. Kwa kumtegemea Mungu akatoka Misri, asiyaogope makali ya mfalme, kwani yeye asiyeonekana alishikamana naye, kama anamwona. Kwa kumtegemea Mungu akaifanya Pasaka na kupaka damu, mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse. Kwa kumtegemea Mungu wakapita katika Bahari Nyekundu, kama ni nchi kavu, lakini Wamisri walipovijaribu wakatoswa. Kwa hivyo, Waisiraeli walivyomtegemea Mungu, maboma ya Yeriko yakaanguka yalipozungukwa siku saba. Kwa kumtegemea Mungu Rahabu, angawa alikuwa mwanamke mgoni, hakuangamia pamoja na wale wasiotii, maana wale wapelelezi aliwapokea na kuwatuliza mioyo. Nisemeje tena? Kwani saa hazingenitosha, kama ningeyasimulia mambo ya Gideoni na ya Baraka na ya Samusoni na ya Yefuta na ya Dawidi na ya Samweli na ya wafumbuaji. Hao kwa kumtegemea Mungu walipigana na wafalme, wakawashinda, wakaamua kwa wongofu, wakaona, viagio vilivyotimia, wakavifunga vinywa vya simba, wakazima mioto yenye nguvu, wakapona ukali wa panga. Walipokuwa wanyonge walipewa nguvu tena, wakawa wakali vitani, wakakimbiza vikosi vizima vya wageni. Kwa kufufuka kwao, ambao walifiwa nao, wanawake waliwapata tena wao hao, waliofiwa nao. Lakini wengine walipoteswa walitaka kuuawa, wakakataa kukombolewa, wapate ufufuko ulio mzuri uliko huo. Wengine walijaribiwa na kufyozwa pamoja na kupigwa, wengine wakafungwa minyororo, wakatiwa vifungoni. Waliuawa kwa kupigwa mawe, walipondwa, walipasuliwa, walikufa kwa kuchomwa majisu, walifukuzwa po pote, wajiendee wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi tu, wakiwa na njaa, wakiumia kwa maovu, waliyofanyiziwa. Kweli haikuupasa ulimwengu huu kuwa nao, wakatangatanga maporini na milimani na mapangoni na mashimoni ndani ya nchi. Hao wote walipoteseka, ndipo, walipotimiza kumtegemea Mungu, lakini hawakuona, kiagio kilivyotimia. Kwani Mungu alikuwa ametupatia kale kitu kilicho kizuri sana, maana wale wasipate kutimilika pasipo sisi. *Kwa sababu tuna mashahidi walio wengi hivyo, wanaotuzunguka, kama ni wingu, na tuyatue yote yatulemeayo, tujitenge na makosa yanayoshikamana nasi! Tena katika mashindano, tuliyo nayo, na tukikimbilie kikomo na kuvumilia tukiyaelekeza macho kwake Yesu, maana ndiye aliyetuanzisha kumtegemea, tena ndiye anayetaka kukutimiliza. Yeye akayaacha yaliyoufurahisha moyo wake, akajitwika msalaba, pasipo kuona soni. Kisha akaketi kuumeni penye kiti cha kifalme cha Mungu. Mkumbukeni aliyevumilia alipobishiwa hivyo na wakosaji, msipate kuchoka mioyoni mwenu wala kulegea! Hapo, mnapopigania kushinda makosa, hamjajifikisha kwenye kuuawa na kumwagwa damu. Nanyi mmeyasahau matulizo ya mioyo, aliyotuambia, ya kama tu wana wake kwamba: Mwanangu, usiseme: Si kitu, ukichapwa na Bwana, wala usilegee, unapokanywa naye! Kwani Bwana humchapa anayempenda, naye humpiga kila mwana, anayempokea.* Vumilieni, mwonyeke! Mungu huwatunza kama wanawe. Kwani ni mwana gani, baba yake asiyempiga? Lakini mkiwa hampigwi, kama wote walivyopigwa, basi, ninyi m wana wa kitumwa, ham wana wa kiungwana. Tena, tukiwa tumepigwa na baba zetu waliotuzaa, tukaonyeka, je? Hatutajikaza sana kumtii Baba aliyezizaa roho zetu, tupate kuishi? Kwani wale waliotupiga siku chache, kama walivyowaza wenyewe kuwa vema. Lakini huyo hutupigia yafaayo, tugawiwe naye utakatifu wake. Mapigo yote, yanapokuwapo, hatuyawazii kuwa furaha, ila masikitiko. Lakini siku za nyuma wale waliofundishwa nayo huona, yanavyowazalia matunda yenye utengemano na wongofu. *Kwa hiyo mikono iliyolegea nayo magoti yaliyopooza yatieni nguvu tena! Nayo miguu yenu ishikisheni mapito yaliyo malinganifu! Maana wachechemeao wasipotezwe, ila wapate kupona vema! Kukimbilieni kupatana nao watu wote! Tena ukimbilieni utakaso! Kwani hata mmoja hatammwona Bwana asipokuwa ametakaswa. Angalieni, mtu asiyakose mema, Mungu ayagawiayo! Wala pasichipuke shina lenye uchungu, likiwasumbua na kuchafua wengi! Wala kusionekane mwenye ugoni wala mwenye kumbeza Mungu kama Esau aliyeuuza ukubwa wake kwa chakula kimoja! Kwani mnajua, hapo nyuma, alipotaka kuirithi mbaraka, alitupwa. Kwani hakupata tena penye kujutia, angawa alipatafuta sana kwa machozi.* *Kwani hamkufika penye mlima uliogusika, ukiwaka moto, wala penye wingu jeusi na giza na upepo mkali, wala penye mlio wa baragumu na uvumi wa maneno yaliyowashinda wenye kuyasikia, wakaomba, wasiambiwe tena neno. Kwani hawakuweza kulipokea lile agizo la kwamba: Hata nyama atakayeugusa mlima auawe kwa kupigwa mawe au kwa kuchomwa mikuki. Nayo yaliyoonekana yalikuwa yamewatia woga mkubwa sana, hata Mose akasema, nimeingiwa na kituko, nikatetemeka. Ila mmefika penye mlima wa Sioni, ndipo penye mji wa Mungu Mwenye uzima, ni Yerusalemu ulioko mbinguni, panapo malaika maelfu na maelfu wanaowashangilia wateule waliozaliwa wa kwanza, ndio walioandikwa majina mbinguni. Kisha mmefika penye Mungu aliye mhukumu wa watu wote; ndipo, nazo roho za wenye wongofu waliotimilika zilipo, ndipo, alipo naye Yesu aliyetuletea Agano Jipya, hata damu ya kunyunyizia inayosema na nguvu kuipita ile ya Abeli ipo papo hapo.* Angalieni, msimkataye yeye anayesema! Kwani kama wale waliomkataa, aliposema nao nchini, hawakuweza kukimbia, sisi tutawezaje kukimbia tukijitenga naye, anaposema nasi toka mbinguni? Sauti yake ndiyo iliyoitingisha nchi siku ile; lakini sasa kiko kiagio cha kwamba: Mimi nitatetemesha tena mara moja, si nchi tu, ila hata mbingu. Lakini neno hili la kwamba: Tena mara moja linaeleza, ya kuwa vinavyotingishika hugeuka, kwa kuwa viliumbwa hivyo, kusudi vile visivyotengishika vikae vivyo hivyo. Kwa sababu tumepewa ufalme usiotingishika, na tuyavumishe hayo mema, tuliyogawiwa! Hivyo tutamtambikia Mungu, kama inavyompendeza, tukimcha na kumwogopa. Kwani Mungu wetu ni moto ulao kwa kuteketeza. *Kaeni na kupendana kindugu! Msisahau kuwakaribisha wageni! Kwani hivyo wengine walikaribisha malaika, nao wenyewe hawakuwajua. Mwakumbuke waliofungwa, kama m wafungwa wenzao! Mwakumbuke wenye kufanyiziwa maovu! Maana ninyi wenyewe mmo miilini bado. Unyumba sharti uheshimiwe nao wote, hapo penye kitanda chao wanyumba pasifanywe chochote chenye uchafu. Kwani Mungu atawahukumu wagoni na wazinzi. Msiwe wapenda fedha, mtoshewe nayo yaliyo yenu! Kwani yeye mwenyewe anasema: Sitakuacha, wala sitakuepuka. Kwa hiyo sisi hujipa moyo wa kusema: Bwana akiwa ananisaidia, sitaogopa; maana aliye mtu atanifanyia nini? Mwakumbuke waliowaongoza ninyi, waliowaambia Neno la Mungu! Tazameni, walivyotoka ulimwenguni, mviige, walivyomtegemea Mungu! Yesu Kristo alivyokuwa jana na leo, ndivyo, atakavyokuwa kale na kale. Msijipoteze na kujifunza mafundisho mengi yaliyo mageni! Kwani ni vizuri, moyo ukishupaa kwa kugawiwa nguvu, si kwa miiko ya vyakula; kwani waifuatao hawajipatii chochote.* Sisi tunapo petu pa kutolea vipaji vya tambiko, napo ni penye mwiko wa kuvila kwao watambikiao Hemani. Kwani damu za nyama zikiisha kupelekwa Patakatifu na mtambikaji mkuu kwa ajili ya makosa, basi, miili yao hao nyama huteketezwa nje ya kambi. Kwa hiyo hata Yesu aliteswa nje ya mlango wa mji, awatakase watu kwa damu yake mwenyewe Kwa hiyo tumtokee tukitoka kambini na kuvumilia maumivu yenye soni yalinganayo nayo yake! Kwani huku hatuna mji ukaao, ila tunaufuata ule ujao. Tukiwa naye yeye, tumtolee Mungu po pote vipaji vya tambiko vya kumsifu, ndiyo matunda ya midomo iliungamayo Jina lake! Msisahau kutenda mema na kugawiana na wenzenu yaliyo yenu! Kwani vipaji kama hivyo humpendeza Mungu. Wenye kuwaongoza watiini na kuwanyenyekea! Kwani hao huzikeshea roho zenu, maana ndio watakaoulizwa kwa ajili yao, nao hutaka kuzifanya kazi zao kwa furaha pasipo kupiga kite. Kwani hivi haviwafalii kitu ninyi. Tuombeeni sisi! Kwani mioyo yetu hutushuhudia, tuyajuayo kwamba: Twataka kufanya mwenendo mzuri katika mambo yote. Lakini nakaza kuwahimiza, mfanye hivyo, nirudishwe kwenu upesi. Mungu mwenye utengemano aliyemtoa kwenye wafu Bwana wetu Yesu aliye mchungaji mkuu wa kondoo kwa nguvu ya damu ya Agano la kale na kale, yeye Mungu awape nguvu ya kuyafanya mema yote, ayatakayo! Maana yeye ndiye anayetupa kuyafanya yapendezekayo mbele yake, akitushikisha njia yake Yesu Kristo. Huyu na atukuzwe kale na kale pasipo mwisho! Lakini nawahimiza, ndugu, yatieni mioyoni maneno haya ya kuwaonya! Kwani nimewaandikia na kukatakata. Jueni, ya kuwa ndugu yetu Timoteo amefunguliwa! Akija upesi, tutaonana nanyi pamoja na yeye. Nisalimieni wote wawaongozao na watakatifu wote! Nao wenzetu wa Italia wanawasalimu. Upole uwakalie ninyi nyote! Amin. Mimi Yakobo niliye mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo nawasalimu ninyi mlio mashina kumi na mawili yaliyotawanyika. Ndugu zangu, mnapotumbukia katika majaribu yaliyo mengi na mengi yawazieni kuwa machangamko tu! Yatambueni: Kumtegemea Mungu kukijulishwa hivyo kuwa kwa kweli huwaletea uvumilivu. Nao uvumilivu sharti uitimize kazi yake, ninyi mpate kutimilika, mwe Wakristo wazima wasioachwa nyuma katika jambo lo lote. Lakini kama kwenu yuko akosaye werevu wa kweli, na amwombe Mungu anayependezwa kuwapa watu wote pasipo mawazo ya kinyuma; ndipo, atakapopewa. Lakini sharti aombe kwa kumtegemea, asiwe na mambo mawili moyoni! Kwani mwenye mambo mawili hufanana na wimbi la bahari linalorushwarushwa na upepo na kutupwatupwa. Mtu aliye hivyo asidhani, ya kuwa kiko, atakachokipata kwake Bwana! Mtu mwenye mioyo miwili hugeukageuka katika njia zake zote. Lakini ndugu mnyenyekevu na ajivunie ukuu wake, naye mwenye mali na ajivunie unyenyekevu wake, kwani atanyauka kama maua ya majani. Kwani jua likicha na kuwaka kwa ukali huyakausha majani, maua yaanguke, uzuri wao uliofurahisha macho uangamie. Vivyo hivyo naye mwenye mali hunyauka katika mienendo yake. Mwenye shangwe ni mtu anayevumilia akijaribiwa. Kwani akiisha kushinda atapewa kilemba chenye uzima, Mungu alichowaagia wale wampendao. Mtu akijaribiwa asiseme: Najaribiwa na Mungu! Kwani Mungu hajaribiki nayo maovu, naye mwenyewe hajaribu mtu. Ila kila mtu hujaribiwa akivutwa na kuhimizwa na tamaa yake mwenyewe. Kisha tamaa ikijitunisha huzaa makosa, nayo makosa yakikomaa huzaa kufa. *Msidanganyike, ndugu zangu wapendwa! Kila kipaji kizuri na kila gawio timilifu hutoka juu kwa Baba alie mwenye mianga. Yeye hageuki, wala kwake hakupokeani mwanga na giza. Kwa hayo, ayatakayo, alituzaa sisi kwa nguvu ya Neno lililo kweli, tupate kuwa kama malimbuko ya viumbe vyake. Mwajua, ndugu zangu wapendwa: kila mtu awe mwepesi, apate kusikia, lakini awe mpole, asiseme upesi, tena mpole, asipatwe na makali upesi! Kwani makali ya mtu hayafanyi yaongokayo mbele ya Mungu. Kwa hiyo uvueni uchafu wote na ule uovu mwingi uliowashika! Lipokeeni kwa upole Neno lililopandwa mwenu, liwezalo kuziokoa roho zenu!* *Mwe wafanyaji wa Neno, msiwe wasikiaji tu! Kwani hivyo mwajidanganya wenyewe. Kwani mtu akiwa msikiaji wa Neno, asiwe hata mfanyaji, huyo amefanana na mtu aliyetazama katika kioo, uso wake ulivyo; akiisha kujitazama huenda zake, akasahau upesi, alivyokuwa. Lakini achunguliaye, aone, Maonyo yalivyotimilika hapo, tulipokombolewa, akishikamana navyo, hawezi kuwa msikiaji asahauye upesi, aliyoyasikia, ila huwa mfanyaji wa kazi yake, naye atakuwa mwenye shangwe kwa kule kufanya kwake. Mtu akijiwazia kuwa mwenye kumtumikia Mungu, lakini haushindi ulimi wake, anaudanganya moyo wake mwenyewe, kwa hiyo matumikio yake ni ya bure. Matumikio yatakatayo yasiyo yenye doa hata machoni pa Mungu Baba ndiyo haya: kukagua watoto waliofiwa na wazazi na kukagua nao wanawake wajane katika maumivu yao na kujilinda wenyewe, tusijitie katika machafu ya ulimwwengu huu.* Ndugu zangu, msiwaze kwamba: Kumtegemea Bwana wetu mtukufu Yesu Kristo hupatana na kupendelea watu! Ni hivyo: mle mkutaniamo mkiingia mtu mwenye pete za dhahabu vidoleni, aliyevaa mavazi mazuri, tena mkiingia hata maskini mwenye mavazi machakavu, nanyi mkamtazama yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia: Wewe kaa hapa pazuri! kisha mkamwambia yule maskini: Wewe simama huko au kaa hapa chini miguuni pangu! je? Hivyo mioyo yenu haikujiumbua kwamba: Mkiwagawanya hivyo mmefuata mawazo mabaya? Sikilizeni, ndugu zangu wapendwa! Mungu hakuwachagua walio maskini ulimwenguni, wawe wenye mali kwa kumtegemea, tena wautwae ufalme, aliowaagia wampendao, uwe urithi wao? Lakini ninyi mmemnyima maskini heshima. Wenye mali sio wanaowaendea ninyi kwa nguvu? Sio wanaowaburura bomani? Nao sio wanaolitukana lile Jina zuri, mwitwalo nalo? Kweli, mkilitimiza Agano la kifalme, kama lilivyoandikwa kwamba: Umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwenyewe! mnafanya vizuri. Lakini mkiwapendelea watu mnakosa, mkajulishwa na hilo agizo waziwazi kuwa wenye kulipita. *Kwani mtu akiyashika Maonyo yote akalikosea moja tu, amekwisha kuyakosea yote. Kwani yeye aliyesema: Usizini! ndiye aliyesema: Usiue! Nawe usipozini, lakini unaua, basi, umekwisha kuwa mwenye kuyapita Maonyo. Semeni, tena fanyeni hivyo, kama watu wafanyavyo watakaohukumiwa kwa Maonyo yanayotupatia kukombolewa! Kwani mtu akosaye huruma atapata naye hukumu ikosayo huruma; lakini huruma hushangilia nako kwenye hukumu. Ndugu zangu, mtu akisema: Niko na kumtegemea Mungu, lakini matendo hanayo, inamfaliaje? Kumtegemea Mungu kunaweza kumwokoa? Kwetu kukipatikana ndugu mume au mke walio wenye uchi na wenye kukosa chakula cha siku moja tu, mtu wa kwenu akawaambia: Nendeni na kutengemana, mwote moto, mpate kushiba! asiwape yaipasayo miili yao, itawafaliaje? Hapo mwaona: Kumtegemea Mungu kusikoendelea na matendo yakupasayo kumekwisha kuangamika kwenyewe.* Labda yuko atakayesema: Wewe uko na kumtegemea Mungu, nami niko na matendo; nionyesha, unavyomtegemea Mungu pasipo matendo! kisha nami nitakuonyesha, matendo yangu yanavyotimilika katika kumtegemea Mungu. Wewe unaamini, ya kuwa Mungu ni mmoja tu? Ni vizuri; pepo nao huyaamini hayo, lakini hutetemeka! Mtu mpuzi, unataka kutambua, ya kuwa kumtegemea Mungu kusikoendelea na matendo ni kwa bure? Baba yetu Aburahamu hakupata wongofu kwa matendo alipompeleka mwana wake Isaka, awe ng'ombe ya tambiko? Unaona: Kumtegemea Mungu husaidiana na matendo yakupasayo; napo, alipofanya yampasayo, ndipo, kumtegemea Mungu kulipotimilika kwake, nayo yaliyoandikwa yakatimia kwamba: Aburahamu alimtegemea Mungu, kwa hiyo akawaziwa kuwa mwenye wongofu, akaitwa mpenzi wake Mungu. Mnaona: Mtu hupata wongofu kwa matendo, siko kwa kumtegemea Mungu tu. Tena je? Yule mke mgoni Rahabu hakupata wongofu naye kwa matendo, alipowafikiza wale wajumbe na kuwatoa mjini kwa njia nyingine? Kwani kama mwili unavyokufa, usipopumua, vivyo hivyo nako kumtegemea Mungu kusikoendelea na matendo kunakufa. Ndugu zangu, haifai, wengi wakiwa wafunzi. Jueni: hukumu, tutakayoipata sisi, itakuwa kuliko ya wengine! Kwani sisi sote hukosa mengi. Mtu asipokosa kwa kusema, huyo ni mume mtimilifu anayeweza kuuongoza hata mwili wote. Tazameni, farasi twawatia hatamu vinywani, watutii sisi; nasi hivyo huwaongoza miili yao yote kwenda huko, tunakopenda. Tazameni, hata merikebu zilivyo kubwa sana, tena zinavyochukuliwa na pepo zenye nguvu! Nazo huongozwa na sukani iliyo ndogo sana, mwenye kuishika anakotaka. Vivyo hivyo nao ulimi ni kiungo kidogo, nao hujivunia makuu! Tazameni, moto ulio mdogo huchoma pori kubwa! Nao ulimi ni moto, ni ulimwengu wenye upotovu. Katika viungo vyetu ndio ulimi unaouchafua mwili wote, unavichoma vyote vilivyoumbwa, wenyewe ukiwashwa na moto ulioko kuzimuni. Kwani nyama wo wote, kama nyama wa porini na ndege na nyoka na nyama wa baharini, wote hufugika, nao wamekwisha fugwa na nguvu za watu. Lakini huo ulimi hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu yenye kuua. Ndio, unaotutukuzisha Bwana aliye Baba, tena ndio, unaotuapizisha watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu. Matukuzo na maapizo hutoka katika kinywa kilekile kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapasi kuwa hivyo. Je? Iko chemchemi inayotoa maji matamu na machungu katika kisima kilekile kimoja? Ndugu zangu, uko mkuyu unaoweza kuzaa chikichi, au mzabibu unaoweza kuzaa kuyu? Napo penye chumvi hapatoki maji matamu. Kwenu yuko nani aliye mwerevu wa kweli wa kujua mambo? Ajionyeshe kuwa mwenye mwenendo mzuri, nazo kazi zake zijulike kuwa zenye upole utokao katika huo werevu wa kweli! Lakini mkiwa wenye wivu ulio na uchungu na wenye uchokozi mioyoni mwenu msijivune, wala yaliyo ya kweli msiyageuze kuwa uwongo! Kwani werevu huu haukutoka mbinguni juu, ila nchini, ni wa kimtu na wa Kisatani. Kwani wivu na uchokozi ulipo, ndipo palipo penye matata na mambo maovu yo yote. Lakini werevu wa kweli utokao mbinguni juu kwanza ni wenye ung'avu, kisha ni wenye utengemano na upole na unyenyekevu, huwahurumia wote na kuwapatia mazao mema; haupendelei, maana hukataa ujanja. Nalo tunda la kuzaa wongofu hupandwa nao wenye utengemano panapotengemana. Magomvi yenu ya kupigana ninyi kwa ninyi yanatoka wapi? Sipo hapo, mzichezeapo tamaa zenu zinazoshindana katika viungo vyenu? Mwakifuata kijicho, lakini hampati; mwauana kwa wivu, lakini hamwezi kuyafikia, myatakayo; mwapigana na kugombana, lakini hamna kitu, kwa sababu hamwombi. Mngawa mwaomba, lakini hampewi, kwa sababu mwaomba vibaya, maana mwataka tu ya kutumia katika machezo yenu. Enyi wazinzi waume na wanawake, hamjui: kuupenda ulimwengu huu ni kuchukiwa naye Mungu? Anayetaka kuwa mpenzi wa ulimwengu huu, hugeuka kuwa mchukivu wa Mungu. Au mwawaza, ya kuwa Maandiko yanasema bure: Roho aliyekaa ndani yetu anataka sana kushindana na wivu? Nayo mema, atugawiayo, ni makubwa kuushinda. Kwa hiyo maandiko yasema: Wenye kujikweza Mungu huwapingia, lakini wanyenyekevu huwapatia huruma. Kwa hiyo mtiini Mungu! Satani mbisheni! Ndivyo, atakavyowakimbia. Mkaribieni Mungu! Ndivyo, atakavyowakaribia nanyi. Enyi wakosaji, ing'azeni mikono! Enyi wenye mioyo miwili, itakaseni mioyo! Jisumbueni na kusikitika na kuomboleza! Macheko yenu yageuke kuwa vilio, nazo furaha zenu zigeuke kuwa masikitiko! Mjinyenyekeze mbele ya Bwana! Ndivyo, atakavyowakuza ninyi. Msitetane, ndugu! Anayemteta ndugu au anayemwumbua ndugu yake huyateta Maonyo na kuyaumbua Maonyo. Lakini ukiyaumbua hu mfanyaji wa Maonyo, ila muumbuzi. Mwenye kuyatoa Maonyo na mwenye kuhukumu ni mmoja, maana ni yeye anayeweza kuokoa na kuangamiza. Lakini wewe u nani ukimwumbua mwenzio? *Sasa tusemeane nanyi mnaosema: Leo au kesho tutakwenda mjini fulani, tukae huko mwaka mzima, tuchuuze na kuchuma! Nanyi hamjui, itakayokuwa kesho. Kuishi kwenu ni kwa namna gani? Maana ninyi m kama mvuke unaoonekana kitambo kidogo, kisha hutoweka. Mngesema: Bwana akitaka, tutaishi, tufanye hivi na hivi. Lakini sasa mwajivunia kwa kujitutumua; majivuno yote yaliyo hivyo ni mabaya. Ajuaye kufanya mazuri, asiyafanye, amekwisha kukosa.* Sasa tusemeane nanyi wenye mali: Lieni na kuyaombolezea mahangaiko yenu yatakayowapata! Mali zenu zimeoza, nguo zenu zimeliwa na mende. Dhahabu zenu na fedha zenu zimeingiwa na kutu, nazo kutu zao zitawasuta, zitawala nyama za miili yenu kama moto. Mmelimbika mali nyingi siku hizi za mwisho. Angalieni, malipo, mliyowanyima wakulima wa mashambani kwenu, yanalia, nayo malalamiko ya wavunaji yamefika masikioni mwa Bwana Mwenye vikosi. Mmeyala mazuri yaliyoko nchini na kutapanya mali. Mioyo yenu mmeinonesha siku za kuchinja nyama. Mwongofu mmemhukumu, mkamwua; naye hakuwabishia. Ndugu, vumilieni, mpaka Bwana atakaporudi! Tazameni, mkulima anavyoyangoja mazao ya nchi, maana ni yenye kima! Huvumilia mpaka apate mvua ya vuli nayo ya masika. Vumilieni nanyi, mwitie mioyo yenu nguvu! Kwani kurudi kwake Bwana kumekaribia. Ndugu, msinung'unikiane ninyi kwa ninyi, msipate kuhukumiwa! Tazameni, mhukumu amesimama milangoni mwenu! Ndugu, wafumbuaji waliosema kwa nguvu ya Jina la Bwana washikeni kuwa vielezo vya kujifunzia kuteseka vibaya na kuvumilia! Tazameni, twawatazamia wavumiliao kuwa wenye shangwe! Mmesikia, Iyobu alivyovumilia, nao mwisho wa Bwana mmeuona, kwani Bwana huonea wengi uchungu na upole. Ndugu zangu, nilitakalo sana, ni hili la kwamba: Msiape! Msiape na kutaja wala mbingu wala nchi wala kiapo kingine cho chote! Mkisema: Ndio, iwe ndio kweli. Tena mkisema: Sio, iwe sio kweli, kwamba msitumbukie hukumuni! *Kwenu kama yuko mwenye kuteseka, na amwombe Mungu! Kama yuko mwenye kutulia, na aimbe nyimbo! Kama yuko mwenye kuugua, na awaite wazee wa wateule, wamwombee, tena wampake mafuta katika Jina la Bwana! Wakimwombea kwa kumtegemea Mungu, vitamwokoa yule mgonjwa, naye Bwana atamwinua tena; kama yuko na makosa, aliyoyafanya, ataondolewa. Jiungamianeni makosa ninyi kwa ninyi na kuombeana, mpate kupona! Kuomba kwake mwongofu kuko na nguvu nyingi kukiwa kwa kweli. Elia alikuwa mtu aliyeteseka kama sisi; naye alipomwomba Mungu, mvua isinye, ndipo, mvua ilipoacha kunya nchini miaka mitatu na miezi sita. Alipoomba tena, ndipo, mbingu ziliponyesha mvua, nayo nchi ikayachipuza mazao yake. Ndugu zangu, kama kwenu yuko aliyepotea na kuyaacha yaliyo ya kweli, tena mwingine akimrudisha, tambueni: mwenye kurudisha mkosaji, aiache ilenjia yake ya upotevu, huiokoa roho yake kufani na kufunika makosa mengi!* Mimi Petero niliye mtumwa wa Yesu Kristo nawaandikia ninyi wateule mkaao ugenini na kutawanyika kule Ponto na Galatia na Kapadokia na Asia na Bitinia. Kwa hivyo, Mungu Baba alivyowatambua kale, aliwatakasa kwa Roho yake, mpate kutii kwa kunyunyizwa damu yake Yesu Kristo. Upole uwafurikie na utengemano! *Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa sababu alituonea huruma nyingi, akatuzaa mara ya pili, tupate kingojeo chenye uzima kwamba: Yesu kristo amefufuka katika wafu! Ndipo, alipotupatia fungu lisiloozeka, lisilochafuka, lisilonyauka; hilo mmelimbikiwa mbinguni ninyi. Tena mkikaa na kumtegemea mnalindwa kwa nguvu za Mungu, mpate wokovu uliotengenezwa wa kutokea waziwazi siku za mwisho. Hapo mtashangilia, hata ikiwapasa sasa kusikitika siku kidogo, mkijaribiwa na mambo menginemengine, kwamba: Kumtegemea Mungu kujulike kwenu kuwa kwa kweli, kisha kuonekane kuwa kwenye kima sana kuliko dhahabu iangamikayo, nayo uzuri wake hujulikana motoni. Mkiwa hivyo mtapata sifa na utukufu na macheo hapo, Yesu Kristo atakapotokea waziwazi. Naye mmempenda pasipo kumwona, mkamtegemea pasipo kumwona kamwe; kwa hiyo mtashangilia kwa furaha isiyosemeka kwa utukufu wake; itakuwa hapo, mtakapoutwaa mwisho wa kumtegemea, ndio wokovu wa roho zenu.* Nao wafumbuaji walioyafumbua hayo mema, mliyogawiwa, waliutafuta sana wokovu huo na kuuchunguza; wakayafuatafuata, wapate kujua, kama ni siku za wakati gani zile, ambazo Roho ya Kristo, waliyokuwa nayo, inazivumbua na kuyashuhudia hapo kale mateso yatakayompata Kristo nao utukufu utakaokuwa mwishoni. Wao walikuwa wamefunuliwa, ya kama mafumbuo yao hayakuwa ya kuwatumikia wao wenyewe, ila ninyi. Nako kwenu yanatangazwa sasa nao wawapigiao hiyo mbiu njema kwa nguvu ya Roho takatifu iliyotumwa toka mbinguni. Basi, mambo hayo hata malaika huyatunukia kuyachungulia. *Kwa hiyo jifungeni kiroho viuno vyenu, mlevuke! Mtimilike na kuyangojea yale mema, mnayoletewa, mgawiwe, Yesu Kristo atakapotokea waziwazi! Kwa sababu m watoto wanaotii, msijielekeze penye tamaa zenu, mlizozifuata hapo kale, mlipokuwa hamjajua maana! Ila kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, vivyo hivyo nanyi mwe watakatifu katika mwenendo wenu wote! Kwani imeandikwa: Mwe watakatifu! Kwani mimi ni mtakatifu.* *Tena ninyi humwita Baba yeye anayemhukumu kila mtu kwa kazi yake pasipo kupendelea; kwa hiyo mwendelee miaka yenu ya kukaa ugenini na kuogopa! Jueni: vyenye kuoza, vingawa fedha au dhahabu, sivyo, ambavyo mlikombolewa navyo katika mwenendo wenu wa kikale uliokuwa hauna maana; ila mmekombolewa kwa damu ya Kristo iliyo yenye kima kikuu, maana alikuwa mwana kondoo asiye na kilema wala doadoa. Alitambulika kale, ulimwengu ulipokuwa haujaumbwa, lakini kutokea alitokea waziwazi siku hizi za nyuma kwa ajili yenu ninyi. Kwake yeye mmepata kumtegemea Mungu aliyemfufua katika wafu na kumpa utukufu kwamba: Awe Mungu tu, mnayemtegemea na kumngojea. Kwa kuwa mmezitakasa roho zenu na kuyatii yaliyo ya kweli, pendaneni kindugu pasipo ujanja mkijikaza kupendana kila mtu na mwenziwe kwa moyo! Kwani mkiwa mmezaliwa mara ya pili, siyo nguvu ya mbegu iozayo, ila ni nguvu ya mbegu isiyoozeka, ndiyo Neno la Mungu lililo lenye uzima, nalo ndilo likaalo. Kwani kila mwenye mwili ni kama majani, nao uzuri wake wote ni kama ua la majani. Majani hunyauka, nayo maua yake hupukutika. Lakini neno lake Bwana hukaa kale na kale. Basi, hilo ndilo neno la mbiu njema, mpigiwayo ninyi.* *Jivueni uovu wote na udanganyi wote na ujanja na kijicho na mateto yote! Kwa kuwa m vitoto vichanga vilivyozaliwa siku hizi, yatakeni maziwa ya kweli yasiyodanganya, mkuzwe nayo, mpaka mwufikie wokovu, mkiwa mmeonja, mkaona, ya kuwa Bwana ni mwema! Huyu mjieni! Maana ni jiwe lenye uzima. Kweli watu walilikataa, lakini Mungu amelichagua kuwa lenye heshima. Nanyi mlio kama mawe yenye uzima mjengwe kuwa nyumba ya Kiroho, mwe watambikaji watakatifu wa kumtolea Mungu vipaji vya tambiko vya kiroho vimpendezavyo kwa ajili ya Yesu Kristo! Kwa hiyo imeandikwa katika Maandiko kwamba: Tazameni, naweka humu Sioni jiwe la pembeni lililochaguliwa kuwa lenye heshima, naye alitegemeaye hatatwezeka. Kwa hiyo ninyi mlitegemealo hupata heshima, lakini wasiolitegemea jiwe hili, waashi walilolikataa, hilihili huwa kwao jiwe la pembeni kwamba: Ni jiwe la kujigongea na mwamba wa kujikwalia. Nao hujigonga, kwa sababu hawalitii Neno; navyo ndivyo, walivyowekewa. Lakini ninyi m ukoo uliochaguliwa, m watambikaji wa kifalme, m chama kitakatifu, m watu wakombolewao, mpate kuyatangaza mema yake yeye aliyewaita, mtoke gizani, mwingie mwangani mwake mlimo na mastaajabu. Kale hamkuwa ukoo mmoja, lakini sasa mmekuwa ukoo wake Mungu. Tena kale mlikuwa hamjui kuhurumiwa, lakini sasa mmekwisha kuhurumiwa.* *Wapendwa, kwa sababu m wageni wanaopita tu, nawaonya ninyi, mziepuke tamaa za miili zinazozigombanisha roho zenu! Fanyeni mwenendo ulio mzuri kwa wamizimu! Hivyo wale wanaowasingizia ninyi kuwa watenda maovu, wanapoziona kazi zenu nzuri, watamtukuza Mungu siku ile, atakapowatokea kuwakagua. Kwa ajili ya Bwana utiini ukuu wote uliowekwa na watu: Akiwa mfalme, maana huwapita wote! Wakiwa viongozi, maana hutumwa naye kulipiza watenda maovu na kuwapa sifa watenda mema! Nayo ndiyo, Mungu ayatakayo, matendo yenu mema yaunyamazishe upuzi wa watu wajinga. Kwani mmekwisha kukombolewa, lakini huko kukombolewa, msikugeuze kuwa kifuniko cha kuuficha uovu, ila mjulike kuwa watumwa wake Mungu! Wote waheshimuni! Wapendeni ndugu! Mwogopeni Mungu! Mheshimuni mfalme! Ninyi watumishi, watiini mabwana zenu na woga wote! Msiwatii wale tu walio wema na wapole, ila nao walio wakali! Kwani huko ni kugawiwa chema, mtu ateswaye kwa kupotolewa akiyavumilia hayo masikitiko kwa kuwa wake Mungu. Kwani ni chema gani cha kukivumisha, mkiyavumilia mapigo, myapatayo kwa sababu ya kukosa? Lakini mkiyavumilia mateso yawapatayo kwa sababu ya kutenda mema, hiki ndicho chema, Mungu alichowagawia.* *Maana ndiyo mliyoitiwa. Kwani Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachilia kielezo, mpate kufuata nyayo zake. Yeye hakufanya lenye kukosa, uwongo tu haukuonekana kinywani mwake. Alipotukanwa hakutukana naye, alipoteseka hakutisha, ila aliyapeleka kwake yeye anayehukumu kwa kweli. Aliyachukua mwenyewe makosa yetu, nao mwili wake ndio ulioyakweza mtini, sisi tupate kuyaepuka makosa na kuukalia wongofu, namo katika mavilio yake ndimo, mlimoponea. Kwani mlikuwa kama kondoo waliopotea. Lakini sasa mmegeuzwa, mmwelekee mchungaji na mkaguzi wa roho zenu.* Vivyo hivyo nanyi wake sharti mwatii waume wenu! Maana kama wako wasiolitii Neno, watatekwa kwa mwenendo wa wake zao pasipo kuambiwa maneno, wakiona kwa macho yao, mnavyoendelea king'avu kwa kuwaogopa. Nayo marembo yao yasiwe ya miili, kama misuko ya nywele na mapambo ya dhahabu na mavazi ya nguo nzuri! Ila uzuri wao uwe wa mioyoni unaojificha mle ndani pasipo kuangamia, maana ni wa mtu mwenye roho ya upole na ya utulivu, naye Mungu huuona kuwa mali kweli. Kwani hata kale wanawake watakatifu waliomngojea Mungu walijipamba hivyo wakiwatii waume wao, kama Sara alivyomtii Aburahamu akimwita bwana. Nanyi wanawake, mnakuwa watoto wake mkitenda mema pasipo kuogopa vituko vyo vyote. Vilevile nanyi waume, mwendeleane na wake zenu na kuwatambua kuwa viumbe vinyonge kuliko ninyi! Tena waheshimuni! Maana nao watagawiwa urithi wao wa uzimani pamoja nanyi; fanyeni hivyo, msizuiliwe kuomba! *Kisha nyote mioyo yenu sharti iwe mmoja, mpate kuvumiliana na kupendana kama ndugu walio wenye uororo na unyenyekevu! Msimlipe mtu uovu kwa uovu, wala matukano kwa matukano! Ila wafanyao hivyo mwaombee mema! Kwani hayo ndiyo, mliyoitiwa, mwirithi mbaraka. Maana atakayependa kuwa uzimani naye atakaye kuona siku njema aulindie ulimi wake, usiseme mabaya, nayo midomo yake, isiseme madanganyifu! Yaliyo mabaya ayaepuke, afanye mema, atafute penye utengemano, apakimbilie! Maana macho ya Bwana huwatazama walio waongofu, masikio yake huyasikia maombo yao. Lakini uso wa Bwana huwapingia wafanyao mabaya. Yuko nani atakayewaponza ninyi, mkijikaza kufanya mema? Lakini ijapo mteswe kwa ajili ya wongofu mtakuwa wenye shangwe. Lakini msiyaogope maogopesho yao, wala msiyahangaikie! Ila mtakaseni Bwana Kristo mioyoni mwenu!* Tena po pote mwe tayari kumjibu kila mtu anayewauliza kwa ajili ya kingojeo chenu kilichomo mwenu! Lakini wajibuni kwa upole na kuwaogopa! Mioyo yenu sharti ijulike kuwa miema! Hivyo wenye kuwasengenya kwamba: M waovu, wataingiwa na soni kwa ajili ya mwenendo wenu, ukiwa mzuri kwa nguvu ya Kristo. Kwani kuteswa kwa ajili ya kutenda mema, Mungu akivitaka, ni vizuri kuliko kuteswa kwa ajili ya kutenda maovu. Kwani naye Kristo alikufa mara moja kwa ajili ya makosa yetu; yeye aliyekuwa mwongofu alikufa kwa ajili yetu tulio wapotovu, atupeleke kwake Mungu. Aliuawa kimwili, lakini alirudishwa uzimani Kiroho. Hapo aliwaendea wazimu nao mle, waliomo kifungoni, akawapigia mbiu wale waliokataa kutii kale, Mungu alipowangoja na kuwavumilia siku zile za Noa, kile chombo kikubwa kilipotengenezwa; lakini miongoni mwao wakaokoka wachache, watu wanane tu katika kondo ile ya maji. Maji hayo ni mfano wa maji ya ubatizo yanayowaokoa sasa hata ninyi; kweli hayaondoi machafu ya miili, ila ya mioyo, ipate kuwa miema na kupatana naye Mungu kwa nguvu ya ufufuko wake Yesu Kristo. Yeye yuko kuumeni kwa Mungu, maana amekwenda mbinguni, atiiwe nao malaika na wenye nguvu na wenye uwezo. Kwa sababu Kristo aliteswa mwilini kwa ajili yetu, jipeni nanyi mioyo iliyo hivyo, iwashindishe! Kwani atesekaye mwilini huacha kukosa, nazo siku zake zilizosalia za kuwapo mwilini hatazimaliza na kuzifuata tamaa za watu, ila atafanya, Mungu ayatakayo. Kwani inatosha, ya kuwa siku zilizopita mmeyafanya, wamizimu wayatakayo, mkifuata uasherati na tamaa na ulevi na ulafi na unywaji na matambiko ya vinyago yamchukizayo Mungu. Wale wanayastukia, ya kuwa sasa hamfuatani nao na kujipujua pasipo kiasi; kwa hiyo wanawatukana. Lakini atakayewalipiza ni yeye aliye tayari kuwahukumu wanaoishi nao waliokufa. Kwani kwa hiyo hata wafu walipigiwa mbiu njema, wahukumiwe kimwili, kama iwapasavyo watu, kisha wapate kuwapo kiroho, kama Mungu anavyokuwapo. Mwisho wa vitu vyote uko karibu. Kwa hiyo mjiangalie, mlevuke, mpate kuomba! *Lakini kupita yote: jikazeni kupendana wenyewe! Kwani upendano hufunika makosa mengi. Mkaribishane pasipo kunung'unika! Mtumikiane ninyi kwa ninyi, kila mtu akikitumia chema chake, alichogawiwa! Hivyo mtakuwa watunzaji wazuri wa yale mema mengi ya Mungu. Mtu akisema na ayaseme, kama ni kusema maneno ya Mungu! Mtu akitumika na atumike kwa kuwa mtu aliyepewa nguvu na Mungu kwamba: Katika mambo yote Mungu atukuzwe kwa ajili ya Yesu Kristo! Wake yeye ni utukufu na uwezo kale na kale pasipo mwisho! Amin.* *Wapendwa, msistuke kama wenye kuona neno geni mkipatwa na mambo yenye moto! Maana mtajaribiwa tu. Ila mkiwa wenzake Kristo wa kuteseka changamkeni! Maana hapo, utukufu wake utakapotokea waziwazi, ndipo, mtakapochangamka na kushangilia. M wenye shangwe mkitukanwa kwa kuwa mnalo Jina lake Kristo. Kwani Roho wa utukufu na na wa Mungu anawakalia. Lakini kwenu asioneke ateswaye kwa kuwa mwuaji au mwizi au mtenda maovu au mkaguzi wa mambo yasiyo yake! Lakini mtu akiteseka kwa kuwa Mkristo, asione soni, ila amtukuze Mungu kwa kuwamo katika Jina hili! Kwani siku zimetimia, hukumu ianze kwao walio wa Nyumba ya Mungu. Basi, ikianza kwetu itakuwaje mwishoni kwao waliokataa kutii Utume mwema wa Mungu? Tena mwongofu akiona: kuokoka ni kugumu, asiyemcha Mungu na mkosaji atapona wapi? Kwa hiyo nasema: Wenye kuteseka kwa hayo, Mungu aliyoyataka, watende mema! Hivyo wataweza kumwagizia yeye roho zao, maana ni muumbaji mwelekevu.* Wazee walioko kwenu nawaonya mimi niliye mzee mwenzao na shahidi wa mateso yake Kristo, nitakayekuwa mwenziwe hata katika utukufu utakaofunuliwa. Nawaonya kwamba: Lichungeni kundi la Mungu lililoko kwenu, si kwa shuruti, ila kwa kuyapenda wenyewe, Mungu ayatakayo, wala si kwa kufuata machumo mabaya, ila kwa mioyo! Msiwatawale wateule, ila mwe vielezo vya kikundi cha kwenu! Mkiwa hivyo mtapewa kilemba chenye utukufu kisichonyauka, hapo, mchungaji mkuu atakapotokea waziwazi. Vilevile ninyi mlio watu wazima, watiini wazee!* Nyote tumikianeni kila mtu na mwenziwe, kama ni mtumwa wake kwa kujinyenyekeza! Kwani wenye kujikweza Mungu huwapingia, lakini wanyenyekevu huwapatia huruma. Kwa hiyo unyenyekeeni mkono wa Mungu ulio wenye nguvu, yeye awakweze, siku yake itakapofika! Mtupieni Mungu yote, myahangaikiayo! Kwani yeye huwatunza. Levukeni, mkeshe! Kwani mpingani wenu Satani huzunguka kama simba anayenguruma akitafuta, atakayemmeza. Huyo mgombanisheni kwa nguvu ya kumtegemea Mungu mkijua, ya kuwa mateso yayo hayo huwapata nao ndugu zenu walioko ulimwenguni! Naye Mungu mwenye mema yote ya kuwagawia, aliyewaitia nanyi utukufu wake wa kale na kale uliomo katika Kristo, atawalinganya mwenyewe, mkiteseka kidogo, na kuwapa uwezo na nguvu na msingi mgumu. Wake yeye ni utukufu na uwezo kale na kale pasipo mwisho! Amin.* Nimewaandikia kidogo kwa mkono wa ndugu Silwano, ninayemwona kuwa mwelekevu. Nimewaonya na kuwashuhudia kwamba: Mmegawiwa mema ya Mungu yaliyo ya kweli. Nayo yakalieni! Wateule waliomo humu Babiloni pamoja nasi wanawasalimu, hata mwanangu Marko. Mwamkiane na kunoneana kwa kupendana! Utengemano uwakalie nyote mlio wake Kristo! Mimi Simoni Petero niliye mtumwa na mtume wa Yesu Kristo nawaandikia, ninyi myategemeayo pamoja na sisi yale makuu, tuliyopewa kwa wongofu wa Mungu wetu na wa mwokozi Yesu Kristo: Upole na utengemano uwafurikie, mkimtambua Mungu na Bwana wetu Yesu! *Yenye nguvu ya Kimungu yapayo watu kuwapo na kumcha Mungu tumegawiwa yote hapo, tulipomtambua yeye aliyetuitia utukufu na wema wake mwenyewe. Kisha tukagawiwa viagio vikubwa mno vya kutupa macheo kwamba: Kwa nguvu zao mtakuwa, kama Mungu alivyo, mkiyakimbia yanayowaozesha ulimwenguni, ndiyo tamaa za miili. Kwa hiyo jipingieni kwa nguvu zote, hivyo, mnavyomtegemea Mungu, viwapatie wema, nao wema uwapatie utambuzi; nao utambuzi uwapatie kujishinda wenyewe, nako kujishinda kuwapatie uvumilivu, nao uvumilivu uwapatie kumcha Mungu, nako kumcha Mungu kuwapatie kupendana kindugu, nako kupendana kindugu kuwapatie kuwapenda watu wote! Kwani mambo hayo yakiwa kwenu, tena yakiendelea na kufurika, hamtapatwa na uvivu, wala hamtakosa mapato yaliyomo katika utambuzi wa Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini asiye na mambo hayo ni kipofu, haoni, amekwisha kusahau, ya kuwa alitakaswa kwa kuondolewa makosa ya kale. Kwa hiyo, ndugu, jikazeni sanasana kuushupaza wito na uteule wenu! Kwani mkifanya hivyo, hapana tena, mtakapojikwaa. Kwani hivyo mtapewa kuingia kifalme katika ufalme wa Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo ulio wa kale na kale.* Kwa hiyo sitaacha kuwakumbusha mambo hayo siku zote, ijapo mmeyajua, mkaisha kupata nguvu mkiifuata ile kweli, mliyoambiwa. Kwani naona, inafaa kuwakeshesha ninyi na kuwakumbusha mambo hayo siku zote, nikiwa nimo bado katika hema hili. Kwani najua: siku iko karibu, nitakapolitoka hili hema langu, kama alivyonieleza Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini nitawakaza, mweze kuyakumbuka mambo hayo siku zote po pote, hata nitakapokwisha kutoka humu. *Kwani tulipowatambulisha ninyi, uwezo wa Bwana wetu Yesu Kristo utakavyokuwa hapo, atakaporudi, hatukufuata masimulio yaliyotungwa na watu, ila tulikuwa tumeuona ukubwa wake kwa macho yetu wenyewe. Kwani alipopewa heshima na utukufu na Mungu Baba, sauti ilitoka kwenye utukufu mkuu, ikamjia kwamba: Huyu ndiye mwanangu mpendwa, ambaye nimependezwa naye. Nasi tuliisikia sauti hiyo, ilipotoka mbinguni, tulipokuwa pamoja naye juu yake huo mlima mtakatifu. Kwa hiyo tunalishika neno la ufumbuo kwa nguvu sana, nanyi mnafanya vizuri sana mkiliangalia, maana ni mwanga wa kumulikia mahali penye giza, mpaka kutakapokucha, mpaka nyota iwakayo mapema iwatokee mioyoni mwenu. Nalo hili litambueni kwanza, ya kuwa hakuna neno la ufumbuo lililomo Maandikoni, linaloweza kufumbuliwa kimtu tu! Kwani hakuna ufumbuo wo wote ulioletwa kwa hayo, mtu ayatakayo; ila watu watakatifu wa Kimungu waliyasema yaleyale, waliyopewa na Roho takatifu.* Lakini kulikuwako hata wafumbuaji wa uwongo kwao wa ukoo wetu; vivyo hivyo hata kwenu wafunzi wa uwongo watakuwako, wataleta mafundisho wa kuangamiza watu, wamkane naye Bwana aliyewakomboa; hivyo watajiletea wenyewe mwangamizo utakaowafikia upesi. Lakini wengi watayafuata mambo ya uasherati wao, ndio watakaoibezesha njia ya kweli. Kwa choyo chao watawachuuza nanyi na kuwaambia maneno ya udanganyi. Lakini kuhukumiwa kwao hakukawilii tangu kale, nao mwangamizo wao hausinzii. Kwani hata malaika waliokosa Mungu hakuwalimbika, ila aliwakumba kuzimuni, wakiwa wamefungwa na minyororo ya giza, akawatoa, walindwe, mpaka watakapohukumiwa. Nao ulimwengu wa kale hakuulimbika, ila alileta mafuriko ya maji, akayaeneza ulimwenguni kwao wasiomcha Mungu, akamponya Noa tu pamoja na wenzake saba, maana alikuwa mwenye kutangaza wongofu. Nayo miji ya Sodomu na Gomora aliiteketeza kuwa majivu tu; alipoipatiliza hivyo aliiweka kuwa kielezo cha kuwatisha watakaoacha tena kumcha Mungu. Lakini Loti aliyekuwa mwongofu alimwokoa, kwani aliumia sana kwa kuuona mwenendo wao wasioonyeka wakipenda mambo ya uasherati. Kwani huyo mwongofu alikaa katikati yao, nayo matendo mapotovu, aliyoyaona, nayo aliyoyasikia siku kwa siku, yaliuumiza moyo wake mwongofu. Bwana hujua kuwaokoa majaribuni wenye kumcha, lakini wapotovu huwaweka, wapatilizwe siku ya hukumu. Watakaopata makali kupita wengine ndio wale wanaofuata miili migeni kwa kuwa na tamaa chafu; nao ndio wenye kubeza ukuu pasipo kuogopa, hujivuna wenyewe tu, nako kuwatukana wenye utukufu hakuwatetemeshi. Lakini malaika wawapitao uwezo na nguvu hawapeleki masuto ya kuwatukana mbele ya Bwana. Lakini hao hufanana na nyama wasiojua kitu; hao hivyo, walivyoumbwa, huzaliwa, wakamatwe au waoze tu. Vivyo hivyo hata wale watapata kuoza kwa uovu wao, maana huvitukana, wasivyovijua; kisha watalipizwa mapotovu yao. Hushangilia malafi na malevi ya kila siku, huwa kama madoa yachukizayo wakijiingiza kwa udanganyi wao hapo, mnapogawiana vyakula, tena napo hapo hula vibaya. Wana macho yajaayo matongozi, yasiyokoma kukosa; huiponza mioyo ya watu wasioshupaa; mioyo yao huijua mizungu yote ya kuonea mali; maana ni wana wa apizo. Walipoiacha njia iliyonyoka walijipoteza, wakaishika njia ya Bileamu, mwana wa Beori, aliyependa malipo, yangawa mapotovu. Lakini alikemewa alipokataa kuonyeka mwenyewe: punda asiyeweza kusema alisema kwa sauti ya kimtu, akamzuia yeye aliyekuwa mfumbuaji, asifanye lisilofanywa. Hawa huwa kama visima visivyo na maji, tena kama mawingu yanayokimbizwa na ukali wa upepo; fungu lao, walilowekewa, ni lile giza jingi. Husema maneno makuu yasiyo na maana; hivyo, walivyozifuata tamaa za miili na kupitisha kiasi, huwaponza walioanza kuwakimbia wale wanaoendelea kujipoteza. Huwaagia uungwana, nao wenyewe wamo katika utumwa uuao; kwani mtu akitekwa huwa mtumwa wake yeye aliyemteka. Kwani hapo walipomtambua Bwana na mwokozi Yesu Kristo waliyakimbia machafu ya ulimwengu; lakini sasa walipoingia penye matanzi tena wakatekwa, mambo yao ya mwisho yakawa mabaya kuliko ya kwanza. Kwani kama wasingaliitambua njia ya wongofu, ingaliwafalia, kuliko kuitambua, kisha kuliacha tena agizo takatifu, walilopewa. Ilikuwa kwao, kama fumbo la kweli linavyosema: Mbwa huyarudia matapiko yake, naye nguruwe aliyekoga hugaagaa tena matopeni. Wapendwa, barua hii ni ya pili, ninayowaandikia ninyi. Nami katika zote mbili nayakeshesha mawazo yenu yaliyo ya kweli kwa kuwakumbusha: yakumbukeni maneno yaliyosemwa kale na wafumbuaji watakatifu! Tena mlikumbuke nalo agizo la Bwana na mwokozi, mliloambiwa na mitume wenu! *Kwanza litambueni neno hili: siku za mwisho patatokea wafyozaji wenye mafyozi mabaya wanaoendelea na kuzifuata tamaa zao wenyewe wakisema: Kiagio cha kurudi kwake kiko wapi? Kwani tangu hapo, baba zetu walipolala, vyote viko vivyo hivyo, kama vilivyokuwa mwanzoni vilipoumbwa. Nao walio hivyo hawataki kuliona neno hili: mbingu zilikuwako toka kale, nayo nchi ilikuwa imetoka majini kwa neno la Mungu ilishikizika mlemle majini. Kisha ule ulimwengu wa kale uliangamia, ulipofurikiwa na maji. Nazo mbingu za sasa pamoja na nchi zikalimbikwa kwa neno lilelile, zikawekwa, ziteketezwe na moto siku ile, watu wasiomcha Mungu watakapohukumiwa, waangamie. Lakini wapendwa, neno hili moja msilisahau: Kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, nayo miaka elfu ni kama siku moja! Bwana hakawii kukitimiza kiagio, kama wengine wanavyowaza kwamba: Hukawia. Ila huwavumilia ninyi, kwani hataki, wengine waangamie, ila anataka, wote wageuke na kujuta. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi; ndipo, mbingu zitakapotoweka kwa shindo kuu, nayo yaliyoko tangu mwanzo yatayeyuka kwa kuchomwa na moto, hata nchi za kazi zilizomo zitateketezwa. Hizi zote zikienda kuyeyuka hivyo, je? Haiwapasi kuutakasa mwenendo wenu kwa kumcha Mungu? Kisha mwingoje siku ya Bwana, itakapokutia, mpate kumkimbilia, mbingu zitakapoyeyuka kwa kuunguzwa na moto, yaliyoko tangu mwanzo yatakapoteketea kwa kuchomwa na moto! Lakini twatazamia mbingu mpya na nchi mpya zitakazokaa wongofu, kama tulivyoagiwa naye. Kwa hiyo, wapendwa, mkiyatazamia hayo jikazeni, mpate kuonekana kuwa wenye utengemano pasipo kilema wala pasipo doadoa!* Tena uvumilivu wa Bwana wetu mwuwazie kuwa wokovu, kama naye ndugu yetu mpendwa Paulo alivyowaandikia ninyi kwa ujuzi wake, aliopewa. Ndivyo, anavyoandika katika barua zote akiyasema mambo hayo; lakini mle baruani mwake yamo maneno mengine yaliyo magumu ya kuyajua maana. Nao wasiofundishwa vema nao wasiomtegemea Mungu vema huyapindua, kama wanavyoyapindua hata Maandiko mengine; ndivyo, wanavyojiangamiza wenyewe. Basi, ninyi wapendwa mlioanza kuyatambua hayo, jiangalieni, nanyi msipotezwe na upotevu wao wasioonyeka, mkaanguka na kuiacha ngome yenu wenyewe! Ila endeleeni kukuwa mkigawiwa mema, tena mkimtambua Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo! Yeye atukuzwe sasa mpaka siku isiyo na mwisho! Amin. *Yaliyokuwapo tangu mwanzo, tuliyoyasikia, tuliyoyaona kwa macho yetu, tuliyoyatazama na kuyapapasa kwa mikono yetu, ndiyo, tunayoyatangaza kuwa Neno lenye uzima. Nao uzima ulifunuliwa, nasi tukauona, kwa hiyo twashuhudia kwa kuwatangazia ninyi huo uzima wa kale na kale uliokuwa kwa Baba, ukatufunuliwa sisi. Basi, tuliyoyaona, tuliyoyasikia, twawatangazia hata ninyi, nanyi mpate kuwa mwenzetu wa bia. Nayo bia yetu sisi ni ile ya Baba na ya Mwana wake Yesu Kristo. Haya tunawaandikia ninyi, furaha yenu itimizwe.* Nao utume, tuliousikia kwake, tunaowatangazia ninyi, ndio huu: Mungu ni mwanga, namo mwake hamna giza iwayo yote. Tukisema: Tuko na bia naye, kisha tunaendelea gizani, twasema uwongo, nayo yaliyo ya kweli hatuyafanyi. Lakini tukiendelea mwangani, kama yeye alivyo mwangani, tuko na bia yetu sisi kwa sisi, nayo damu ya Yesu, Mwana wake, hututakasa, makosa yote yatutoke. Tukisema: Makosa hatunayo, tunajidanganya wenyewe, nayo kweli haimo mwetu. Lakini tukiyaungama makosa yetu, yeye ni mwelekevu na mwongofu, atuondolee makosa, kisha atutakase, upotovu wote ututoke. Tukisema: Hatukukosa, twamfanya yeye kuwa mwongo, tena Neno lake halimo mwetu. Ninyi vitoto, mlio wangu, haya nawaandikiani, msikose. Lakini kama yuko aliyekosa, tunaye mwombezi kwa Baba, ndiye Yesu Kristo aliye mwongofu. Naye ndiyo kole iliyotolewa kwa ajili ya makosa yetu, lakini si kwa ajili ya makosa yetu tu, ila hata kwa ajili ya makosa ya ulimwengu wote. Namo humu ndimo, tutambuamo, ya kuwa tumemtambua, tukiyashika maagizo yake. Mtu akisema: Nimemtambua, lakini maagizo yake hayashiki, mtu huyo ni mwongo, nayo kweli haimo mwake. Lakini mtu akilishika Neno lake, mwake yeye upendo wa Mungu umetimia kweli. Humu ndimo, tutambuamo, kama tumo mwake. Mtu anayesema: Nafuliza kuwa mwake, huyo inampasa kufanya mwenendo, kama yeye alivyofanya mwenendo. Wapendwa, siwaandikii agizo jipya, ila agizo la kale, mlilokuwa nalo tangu mwanzo. Agizo hilo la kale ndilo Neno, mlilosikia. Tena nawaandikia agizo jipya lililo kweli mwake namo mwenu ninyi, kwamba: Giza hupita, nao mwanga wa kweli umekwisha kumulika. Mtu akisema: Nimo mwangani, akamchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa hivi. Mwenye kumpenda ndugu yake hukaa mwangani, asiwe na kwazo lililomo mwake. Lakini mwenye kumchukia ndugu yake yumo gizani na kuendelea gizani, asijue, anakokwenda, kwani giza imempofusha macho yake. Nawaandikia ninyi mlio vitoto, kwani mmeondolewa makosa yenu kwa ajili ya jina lake. Nawaandikia ninyi mlio baba, kwani mmemtambua yeye aliye mwenye kuwapo tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi mlio vijana, kwani mmemshinda yule Mbaya. Naliwaandikia ninyi mlio wana, kwani mmemtambua Baba. Naliwaandikia ninyi mlio baba, kwani mmemtambua yeye aliye mwenye kuwapo tangu mwanzo. Naliwaandikia ninyi mlio vijana, kwani mko na nguvu, hata Neno la Mungu linakaa mwenu, nanyi mmemshinda yule Mbaya. Msiupende ulimwengu huu, wala vilivyomo ulimwenguni! Mtu akiupenda ulimwengu huu, upendo wa Baba haumo mwake huyo. Kwani vyote vilivyomo ulimwenguni: tamaa za miili nazo tamaa za macho nayo mambo makuu, watu wanayojivunia, havikutoka kwake Baba, ila ulimwenguni. Ulimwengu huu utapita pamoja na tamaa zake; lakini ayafanyaye, Mungu ayatakayo, hukaa kale na kale.* Vitoto, sasa ni saa ya mwisho. Kama mlivyosikia, ya kuwa Mpinga Kristo anakuja, sasa wapinga Kristo wamekwisha kuwapo wengi; kwa hiyo twatambua, ya kuwa ni saa ya mwisho. Walitoka kwetu sisi, lakini hawakuwa wa kwetu; kwani kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka, kusudi waonekane waziwazi, ya kuwa hao wote sio wa kwetu. Nanyi mmemiminiwa mafuta naye aliye Mtakatifu, mkayajua yote. Sikuwaandikia ninyi, kwa sababu hamkuyajua yaliyo ya kweli, ila kwa sababu mmeyajua, tena mmejua, ya kuwa hakuna uwongo utokao kwenye ukweli. Tena yuko nani aliye mwongo, asipokuwa yeye anayekana kwamba: Yesu siye Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo anayemkana Baba na Mwana. Kila anayemkana Mwana hata Baba hanaye vilevile; lakini anayemwungama Mwana anaye hata Baba. Nanyi mliyoyasikia tangu mwanzo, sharti yakae mwenu! Hayo, mliyoyasikia tangu mwanzo, yakikaa mwenu, hata ninyi mtakaa mwake Mwana namo mwake Baba. Nacho kiagio, alichotuagia mwenyewe, ndicho hiki: uzima wa kale na kale. Haya nimewaandikia ninyi kwa ajili yao wanaowapoteza. Yale mafuta, mliyomiminiwa naye, huwakalia, msifundishwe tena na mtu; ila kama mafuta yake yalivyowafundisha mambo yote, ndivyo, yalivyo kweli, huu si uwongo. Kwa hiyo yakalieni, kama yalivyowafundisha ninyi. Sasa, vitoto, kaeni mwake yeye, tupate kushangilia, atakapotokea waziwazi, tusipatwe na soni naye hapo, atakaporudi! Mkijua, ya kuwa yeye ni mwongofu, na mtambue, ya kuwa kila anayefanya wongofu amezaliwa naye yeye! *Tazameni, jinsi Baba alivyotupenda sana, tuitwe watoto wa Mungu! Nasi ndio. Kwa hiyo ulimwengu haututambui, kwani haukumtambua yeye. Wapendwa, sasa tu watoto wa Mungu, lakini havijafunuliwa bado, tutakavyokuwa; twajua tu, ya kuwa vitakapofunuliwa tutafanana naye, tumwone, alivyo. Kila mwenye kumngojea hivyo hujing'aza, kama yeye alivyo mng'avu. Kila mwenye kukosa hukataa kuonyeka, nako kukosa ndiko kukataa kuonyeka. Nanyi mwajua, ya kuwa yule ametokea waziwazi, ayaondoe makosa, maana mwake yeye hamna kosa.* Kila mwenye kukaa mwake hakosi; lakini kila mwenye kukosa hakumwona yeye, wala hakumtambua. Vitoto, pasioneke mwenye kuwapoteza! Mwenye kufanya wongofu ni mwongofu, kama yeye alivyo mwongofu. Mwenye kukosa ametoka kwake Msengenyaji, kwani Msengenyaji hukosa tangu mwanzo. Kwa hiyo mwana wa Mungu alitokea waziwazi, azivunje kazi zake Msengenyaji. Kila aliyezaliwa naye Mungu hakosi, kwani mbegu zake hukaa mwake; kwa hiyo hawezi kukosa, maana alizaliwa naye Mungu. Hapo ndipo panapoonekana wazi walio watoto wa Mungu nao walio watoto wa Msengenyaji: kila asiyefanya wongofu hakutoka kwake Mungu, naye asiyempenda ndugu yake vilevile. Kwani huu ndio utume, mliousikia tangu mwanzo: Tupendane sisi kwa sisi! Tusiwe kama Kaini aliyekuwa wa yule Mbaya, akamwua nduguye. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yeye yalikuwa mabaya, lakini yake nduguye yalikuwa yenye wongofu. *Msistaajabu, ndugu, ulimwengu ukiwachukia ninyi! Sisi twajua, ya kuwa tumetoka kwenye kufa na kuingia kwenye uzima, kwani twawapenda ndugu; asiyewapenda yuko kufani bado. Kila amchukiaye ndugu yake ni mwua watu, nanyi mwajua: hakuna mwua watu aliye mwenye uzima wa kale na kale, atakaoukalia. Hapo ndipo, tulipoutambua upendo: Yeye aliitoa roho yake kwa ajili yetu; nasi imetupasa kuzitoa roho zetu kwa ajili ya ndugu. Lakini mtu mwenye mali za humu ulimwenguni akimtazama tu ndugu yake aliyekosa chakula, akamfungia moyo ake, asimgawie, upendo wa Mungu unamkaliaje? Vitoto, tusipendane kwa maneno, wala kwa ndimi, ila kwa matendo na kwa kweli!* Hapo tutatambua, kama sisi tu wenye kweli, tena hivyo tutaituliza mioyo yetu mbele yake yeye. Kwani mioyo yetu ikituchafukia, Mungu ni mkubwa kuliko mioyo yetu, naye huyatambua yote. Wapendwa, mioyo yetu isipotuchafukia, sisi humshangilia Mungu. Ndipo, tutakapopewa naye lolote, tutakaloliomba, kwani twayashika maagizo yake kwa kuyafanya yanayompendeza. Hili ndilo agizo lake, tulitegemee Jina la Mwana wake Yesu Kristo na kupendana sisi kwa sisi, kama yeye alivyotuagiza. Naye mwenye kuyashika maagizo yake hukaa mwake yeye, naye yeye mwake huyo. Hapo twatambua, ya kuwa yumo mwetu, tukiwa na Roho, aliyetupa sisi. Wapendwa, msiitikie kila roho, ila zijaribuni roho, kama zimetoka kwa Mungu! Kwani wafumbuaji wa uwongo wengi wametokea ulimwenguni. Hapo ndipo, mtakapoitambua roho ya Mungu: kila roho inayoungama, ya kuwa Yesu Kristo amekuja mwenye mwili wa kimtu, imetoka kwa Mungu. Lakini kila roho isiyomwungama Yesu haikutoka kwa Mungu. Hiyo ndiyo roho ya Mpinga Kristo, mliyoisikia, ya kuwa inakuja; tena sasa imekwisha kuwamo humu ulimwenguni. Vitoto, ninyi m wa Kimungu, tena mmewashinda wale, kwani yeye alimo mwenu ni mkubwa kuliko yeye aliomo humu ulimwenguni. Wale ni wa kiulimwengu; kwa hiyo husema ya kiulimwengu, nao wa kiulimwengu huwasikia. Sisi tu wa Kimungu; naye amtambuaye Mungu hutusikia sisi, lakini asiye wa Kimungu hatusikii sisi. Hapo twaitambua roho, kama ni ya kweli au ya upotevu. Wapendwa, tupendane sisi kwa sisi! Kwani upendo ni wa Kimungu. Kila mwenye kupenda amezaliwa naye Mungu, naye humtambua Mungu. Asiyependa hakumtambua Mungu kwamba: Mungu ni upendo. *Upendo wake Mungu wa kutupenda sisi umeonekana waziwazi hapo, Mungu alipomtuma Mwana wake wa pekee kuja ulimwenguni, sisi tupewe naye uzima. Humu ndimo upendo: sio sisi tuliompenda Mungu, ila yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwana wake kuwa kole kwa ajili ya makosa yetu. Wapendwa, kama Mungu alitupenda hivyo, imetupasa nasi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu hata kale; tukipendana, Mungu hukaa mwetu, upendo wake ukatimilika mwetu. Hapa ndipo, tunapotambua, kama tumo mwake yeye, kama yeye naye yumo mwetu, tukiwa na Roho wake, ambaye alitugawia. Nasi tumeviona, tukavishuhudia, ya kuwa Baba amemtuma Mwana, awe mwokozi wa ulimwengu.* Ye yote atakayeungama kwamba: Yesu ni mwana wake Mungu, basi, Mungu hukaa mwake huyo, naye mwake Mungu. Nasi tumeutambua, tukautegemea upendo wake Mungu wa kutupenda sisi. *Mungu ni upendo; naye mwenye upendo hukaa mwake Mungu, naye Mungu hukaa mwake yeye. Upendo, tupendwao nao, unatimilika hapo, tukiweza kuishangilia siku ya hukumu; kwani yeye alivyo, ndivyo, tulivyo na sisi humu ulimwenguni. Woga haumo katika upendo, ila upendo uliotimilika huufukuza woga, kwa sababu woga huhangaisha. Naye aliye mwenye woga bado hajautimiliza upendo. Sisi na tumpende! Kwani yeye alianza kutupenda sisi. Mtu akisema: Nampenda Mungu, akamchukia ndugu yake, huyo ni mwongo. Kwani asipompenda ndugu yake, anayemwona, hawezi kumpenda Mungu, asiyemwona, maana agizo hili tumepewa naye kwamba: Mwenye kumpenda Mungu sharti ampende na ndugu yake!* *Kila mwenye kuyategemea ya kwamba: Yesu ni Kristo, amezaliwa na Mungu. Naye kila mwenye kumpenda mzazi aliyemzaa humpenda hata yeye aliyezaliwa naye. Hapo ndipo, tunapotambua, kama tunawapenda wana wa Mungu, tukimpenda Mungu na kufanya maagizo yake. Kwani kumpenda Mungu ni kuyashika maagizo yake, nayo maagizo yake si magumu. Kwani kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Nako kunakotushindisha ulimwengu ndiko kumtegemea Mungu. Yuko nani anayeushinda ulimwengu, asipokuwa mwenye kuyategemea ya kwamba: Yesu ni Mwana wake Mungu?* Huyu Yesu Kristo ndiye aliyekuja mwenye maji na damu; hakuja na maji tu, ila alikuja mwenye maji na damu. Naye Roho ndiye anayeyashuhudia, kwani Roho ndiye kweli. Kwa hiyo wako watatu wanaoshuhudia mbinguni: Baba na Neno na Roho Mtakatifu; nao hawa watatu ni mmoja. Tena wako watatu wanaoshuhudia nchini: Roho na Maji na Damu; hao watatu nao wamepatana ushahidi kuwa mmoja. *Tukiuitikia ushuhuda wa watu, basi, ushuhuda wa Mungu ni mkubwa zaidi, kwani ushuhuda wa Mungu ndio huo, aliomshuhudia Mwana wake mwenyewe. Mwenye kumtegemea Mwana wa Mungu huo ushuhuda anao mwake. Asiyemtegemea Mungu amemfanya kuwa mwongo yeye, kwani hakuutegemea ushuhuda, Mungu aliomshuhudia Mwana wake mwenyewe. Nao ushuhuda ndio huu wa kwamba: Mungu ametupa uzima wa kale na kale; uzima huu umo mwake Mwana wake yeye. Aliye naye Mwana, anao hata uzima; asiye naye Mwana wa Mungu, hata uzima hanao. Haya nimewaandikia ninyi mnaolitegemea Jina la Mwana wa Mungu, mpate kujua: uzima wa kale na kale mnao. Kunakotupa moyo wa kumjia wenye furaha ndiko kujua, yo yote, tutakayomwomba kwa hayo, ayatakayo, hutusikia. Nasi tukijua, ya kuwa anatusikia yo yote, tutakayomwomba, twajua: maombo, tuliyomwomba, tumekwisha kupewa.* Mtu akimwona ndugu yake, akikosa kosa lisiloua, na amwombee; ndipo, Mungu atakapompa uzima pamoja na wakosaji wenziwe wafanyayo yasiyoua. Liko kosa linaloua; hapo sisemi, mtu amwombee. Upotovu wote ni wa kukosa, tena yako makosa yasiyoua. Twajua: kila aliyezaliwa na Mungu hakosi, ila aliyezaliwa na Mungu hujiangalia, yule Mbaya asimguse. Twajua: sisi tu wa Kimungu, lakini ulimwengu wote umo katika nguvu ya yule Mbaya. Nasi twajua: Mwana wa Mungu amekuja, akatupa mawazo ya kumtambua mwenye kweli. Nasi tumo mwake mwenye kweli, ndimo mwake Yesu Kristo, Mwana wake. Huyu ndiye Mungu wa kweli na uzima wa kale na kale. Vitoto, jiangalieni, msije kutambikia vinyago! Amin. Mimi mzee nakuandikia wewe, mke mkuu uliyechaguliwa, hata watoto wako, ninaowapenda kweli. Lakini si mimi tu ninayewapenda kweli, ila hata wote waliyoyatambua yaliyo ya kweli. Tunawapenda kwa ajili ya kweli ikaayo mwetu, nasi tutakuwa nayo kale na kale. Upole na huruma na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo aliye mwana wa Baba utukalie, tupendane kweli! Nalifurahi sana kwa kuona, wengine walio watoto wako wanavyoishika njia ya kweli, kama tulivyoagizwa na Baba. Hata sasa nakuomba, mke mkuu tupendane; si kama nitakuandikia agizo jipya, ni lilelile, tulilokuwa nalo tangu mwanzo. Nako kupendana ni huko, tukifanya mwenendo, kama alivyotuagiza. Hilo ndilo agizo lake, kama mlivyosikia tangu mwanzo, mwendelee na kulifuata. Kwani wapotevu wengi wametokea ulimwenguni wasioungama kwamba: Yesu Kristo amekuja mwenye mwili wa kimtu. Aliye hivyo ni mpotevu na mpinga Kristo. Jiangalieni, msiyapoteze mapato ya kazi zenu, ila mpewe mshahara wote! Kila anayesogeza mpaka, asikae penye mafundisho ya Kristo, hanaye Mungu; anayekaa penye mafundisho huyu anaye Baba hata Mwana. Mtu akija kwenu asiyeyaleta mafundisho haya, msimpokee nyumbani mwenu, wala salamu msimpe! Kwani mwenye kumsalimia huwa mwenziwe wa kazi zake mbaya. Ninayo mengi ya kuwaandikia ninyi, lakini sikutaka kuyamaliza kwa karatasi na wino, ila nangojea kwamba: Nitakuja kwenu na kusema nanyi kinywa kwa kinywa, furaha yetu itimie. Watoto na dada yako aliyechaguliwa naye wanakusalimu. Amin. Mimi mzee nakuandikia wewe Gayo, mpendwa wangu, ninayempenda kweli. Mpendwa, kuliko yote nakuombea, ukae vema na kuwa mzima, kama roho yako inavyokaa vema. Kwani nalifurahi sana, ndugu walipokuja na kutushuhudia, kuwa u mwenye kweli, kama wewe unavyoishika njia ya kweli. Hakuna linalonifurahisha kuliko lile la kusikia, ya kuwa watoto wangu huishika njia ya kweli. Mpendwa, u mwelekevu katika yote, unayowafanyia ndugu walio wageni. Nao walikushuhudia mbele ya wateule, unavyowapenda. Kwa hiyo utafanya vizuri utakapowasindikiza, kama inavyowapasa walioko mbele ya Mungu. Kwani walitoka kulitangaza Jina lake tu, hawataki kupewa cho chote kwa watu wa kimizimu. Nasi imetupasa kuwapokea watu kama hao, tusaidiane kufanya kazi za kweli. Yako mengine, niliyoyaandikia wateule. Lakini Diotirefe anayependa kuwa mkubwa wao hatusikii sisi. Kwa hiyo nitakapokuja nitazikumbusha kazi zake, anazozifanya akituteta sisi kwa maneno mabaya. Nayo hayo hayamtoshi: mwenyewe hawapokei ndugu, nao wanaotaka kuwapokea huwazuia, kisha huwafukuza kwenye wateule. Mpendwa, usiuige uovu, ila uuige wema! Anayefanya yaliyo mema ni wa Kimungu; anayefanya yaliyo maovu hakumwona Mungu. Lakini Demetirio hushuhudiwa nao wote, naye hushuhudiwa kweli. Hata sisi twamshuhudia, nawe wajua, ya kuwa ushahidi wetu ni wa kweli. Nalikuwa nayo mengi ya kukuandikia, lakini sitaki kukuandikia tu kwa wino na kalamu, ila nangojea, nikuone upesi, tusemeane kinywa kwa kinywa. Utengemano ukukalie! Wapenzi wanakusalimu. Nisalimie wapenzi kila kwa jina lake! Mimi Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo, niliye ndugu wa Yakobo, nawaandikia ninyi mwitwao, mkapendwa kwa kuwa wake Mungu Baba, mkalindwa, mmfikie Kristo. Upole na utengemano na upendo uwafurikie! Wapendwa, nimejikaza sana kuwaandikia ninyi mambo ya wokovu wetu sisi sote, nikashurutishwa moyoni kuwaandikia na kuwahimiza, mlipiganie tegemeo, watakatifu walilokwisha kupewa, liwe lilo hilo. Kwani wako watu waliojiingiza kwa kufichaficha, walivyo, lakini hukumu yao imekwisha kuandikwa kale kwamba: Hawamchi Mungu, maana hupenda uasherati, kisha husema: Mungu wetu hutuondolea hayo, naye yeye aliye mkuu peke yake, Bwana wetu Yesu Kristo humkana. Lakini nataka kuwakumbusha ninyi mliokwisha kuyajua hayo yote: Yeye Bwana aliyewaokoa wao wa ukoo wetu katika nchi ya Misri ndiye aliyewaangamiza waliokataa kumtegemea tena. Hata malaika, wasioulinda ukuu wao wakijiendea na kuyaacha makao yao, amewafunga penye giza kwa mapingu yasiyovunjika, waingoje ile siku kubwa, wahukumiwe. Hata wenyeji wa Sodomu na Gomora nao wa vijiji vilivyokuwako pembenipembeni walihimiza mambo ya ugoni vivyo hivyo na kufuata miili migeni; nalo lipizi lao, walilolipata la kuteketezwa na moto usiozimika, ni kielezo cha kutuonya. Ndivyo, wale wanavyofanana navyo, wako kama wenye ndoto, huichafua miili yao, huutangua ukuu, huwatukana wenye utukufu. Lakini Mikaeli aliye malaika mkuu, aliposhindana na Msengenyaji na kubishana naye kwa ajili ya mwili wa Mose, hakujipa moyo wa kumwumbua na kumtukana, ila alisema tu: Bwana na akukemee! Lakini hao huvitukana, wasivyovijua; navyo vile, wanavyovijua, maana vya miili yao, huvijuaa kama nyama wasiojua kitu, kisha huozeshwa mumo humo. Yatawapata hao, kwani hushika njia ya Kaini, wakapotea na kutumbukia katika mshahara wa Bileamu, wakajiangamiza katika mapingano ya Kora. Hao huwa kama madoa wakijiingiza hapo, mnapogawiana vyakula vya upendano; napo hapo hujilisha wenyewe tu pasipo woga! Tena huwa kama mawingu yasiyo na mvua, yanayochukuliwa na nguvu za upepo, huwa kama miti isiyo na majani, isiyozaa matunda, imekufa mara mbili, imeng'oka kabisa. Tena huwa kama mawimbi makali ya bahari yanayoyatoa mambo yao yaliyo yenye soni kuwa kama mapovu, huwa kama nyota zipoteazo ovyo, ambazo fungu lao, walilowekewa, ni lile giza jingi lililoko kale na kale. Mambo yao aliyafumbua Henoki aliyekuwa mtu wa saba tangu Adamu, aliposema: Tazameni, Bwana anakuja pamoja na malaika zake watakatifu maelfu na maelfu, awahukumu na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya matendo yote, waliyoyafanya kwa kuacha kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote, wakosaji hao wasiomcha Mungu walivyoyasema. Hao hunung'unika na kuchukizwa navyo, waliyoyapata yote, wakiendelea na kuzifuata tamaa zao; vivywa vyao husema maneno makuu, wenyewe hutazama nyuso za watu, waonee ya kupewa. Lakini ninyi, wapendwa, myakumbuke maneno yaliyosemwa kale na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, maana waliwaambia ninyi: Siku za mwisho kutakuwa na wafyozaji watakaoendelea na kuzifuata tamaa zao wenyewe kwa kuacha kumcha Mungu. Hao ndio wanaoleta matengano, ni wa kimtu tu, lakini Roho hawanayo. Lakini ninyi, wapendwa, jijengeni wenyewe mkiyatumia mategemeo yenu matakatifu kuwa msingi! Mwombeni Mungu kwa nguvu ya Roho takatifu! Jilindeni wenyewe, mkae na kumpenda Mungu! Ingojeni huruma ya Bwana wetu Yesu Kristo, itokee na kuwapatia uzima wa kale na kale! Kama wako walio bado wenye mambo mawili, wahurumieni! Waokoeni mkiwapokonya motoni! Lakini wako na wengine, mwahurumie kwa kuogopa! Sharti mchukizwe nazo nguo zao zilizochafuliwa na miili yao! Lakini yeye anaweza kuwalinda, msijikwae, na kuwaweka, mtekee penye utukufu wake na kushangilia kwa kuwa pasipo kilema, yeye ni Mungu peke yake na mwokozi wetu, maana alimtuma Yesu Kristo, Bwana wetu. Utukufu ni wake na ukuu na uwezo na nguvu kuanzia kale, siku zilipoanzia, na sasa na siku zitakazokuwa zote! Amin. Huu ndio ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu, awaonyeshe watumwa wake mambo yatakayo kufanyika upesi. Ndipo, alipomtuma malaika wake, amweleze mtumwa wake Yohana, hayo mambo. Yeye ndiye aliyelishuhudia Neno la Mungu, hata ushuhuda wa Yesu Kristo, maana aliyaona yote. Wenye shangwe ndio wanaoyasoma nao wanaoyasikia maneno ya ufumbuo huu na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwani siku ziko karibu. Mimi Yohana nawasalimu ninyi makundi saba ya wateule yaliyoko Asia. Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwake yeye aliopo, aliyekuwapo, atakayekuja! Tena unatoka nako kwao roho saba walioko mbele ya kiti chake cha kifalme, nako kwa Yesu Kristo; huyu ni shahidi mwelekevu na mzaliwa wa kwanza wa wafu na mkuu wa wafalme wa nchini. Yeye alitupenda, akatukomboa katika makosa yetu kwa damu yake, akatupatia ufalme, tuwe watambikaji wa Baba yake Mungu. Wake yeye ni utukufu na uwezo kale na kale pasio mwisho. Amin. Tazameni, anakuja mawinguni, macho yote yatamwona, nayo yao waliomchoma; ndipo, makabila yote ya nchini yatakapomlilia. Ndio, ni kweli. Mimi ni A na O, ni kwamba: Mwanzo na Mwisho; ndivyo, Bwana Mungu anavyosema aliopo, aliyekuwapo, atakayekuja, aliye Mwenyezi. Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenzenu wa maumivu na wa ufalme na wa uvumilivu, tupewao na Yesu, nilikuwa katika kisiwa kinachoitwa Patimo. Nilikuwako, maana nalilitangaza Neno la Mungu na kumshuhudia Yesu. Nikawapo kiroho penye siku ya Bwana, nikasikia nyuma yangu sauti kuu kama ya baragumu, kwamba: Mimi ni A na O, wa kwanza na wa mwisho; unayoyaona, yaandike katika kitabu, ukitume kwa yale makundi saba ya wateule yaliyoko Efeso na Simirna na Pergamo na Tiatira na Sarde na Filadelfia na Laodikia! Nikapinduka, nione, kama ni sauti ya nani iliyosema nami. Nami nilipopinduka nikaona taa saba za dhahabu. Katikati ya hizo taa nikaona mwenye kufanana na Mwana wa mtu. Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu, napo kifuani alikuwa amejifunga mkanda wa dhahabu. Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba au kama theluji, macho yake yalikuwa kama moto unaowaka. Miguu yake ilifanana na shaba nyekundu imulikayo motoni mwa jikoni, sauti yake ilikuwa kama uvumi wa maji mengi. Namo mkononi mwake mwa kuume alishika nyota saba, namo kinywani mwake mlitoka upanga mkali ulio na makali pande mbili. Nao uso wake ulikuwa kama jua, liking'aa kwa nguvu zake. Nami nilipomwona nikaanguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Ndipo, aliponibandikia mkono wake wa kuume, akasema: Usiogope! Mimi ndiye wa kwanza na wa mwisho na mwenye uzima. Nalikuwa nimekufa, tena tazama, mimi niko, ni mwenye uzima kale na kale pasipo mwisho. Ninazo funguo za kifo na za kuzimu. Basi, yaandike mambo, uliyoyaona, nayo yaliyopo nayo yatakayokuwapo, haya yatakapokwisha! Liandike fumbo la zile nyota saba, ulizoziona mkononi mwangu mwa kuume, nalo fumbo la zile taa saba za dhahabu. Zile nyota saba ndio malaika wa makundi saba ya wateule, nazo taa saba ndio makundi saba ya wateule. Malaika wa wateule walioko Efeso mwandikie: Ndivyo, anavyosema yeye anayezishika zile nyota saba mkononi mwake mwa kuume, anayekwenda katikati ya zile taa saba za dhahabu: Nayajua matendo yako na usumbufu na uvumilivu wako; nakujua: huwezi kuwavumilia waovu, ukawajaribu wale wanaojisema kuwa mitume, lakini sio mitume; nawe uliwaona kuwa waongo. Ukavumilia ulipoumizwa kwa ajili ya Jina langu, hukuchoka. Lakini ninakuonya, ya kuwa umeuacha upendo wako wa kwanza. Kumbuka, uliyoyapoteza ulipoanguka! Kisha juta, uyafanye yale matendo ya kwanza! Usipoyafanya, nitakujia, niiondoe taa yako mahali pake, ukiwa hukujuta. Lakini neno hili unalo, ya kuwa unayachukia matendo yao Wanikolai, ninayoyachukia hata mimi. Mwenye masikio na asikie, Roho anayowaambia wateule! Mwenye kushinda nitampa kula matunda ya mti wa uzima ulioko katika paradiso ya Mungu. *Malaika wa wateule walioko Simirna mwandikie: Ndivyo, anavyosema yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, akapata kuishi tena: Nayajua matendo na maumivu yako na umaskini wako, lakini u mwenye mali nyingi. Nakujua, unavyotukanwa nao wajisemao kuwa Wayuda, lakini sio, ila ni wanafuzi wake Satani. Usiyaogope, utakayoteswa! Tazama, Msengenyaji atawatia wengine wenu kifungoni, mpate kujaribiwa. Nanyi mtaumizwa siku kumi. Uwe mwelekevu mpaka kufa! Ndipo, nitakapokupa kilemba cha uzima. Mwenye masikio na asikie, Roho anayowaambia wateule! Mwenye kushinda hatapotolewa na kufa kwa pili.* Malaika wa wateule walioko Pergamo mwandikie: Ndivyo, anavyosema mwenye ule upanga mkali wenye makali pande mbili: Napajua, unapokaa. Ni hapo, kiti cha kifalme cha Satani kilipo. Lakini unalishika sana Jina langu, hukukana, ya kuwa unanitegemea mimi, hata siku zile, shahidi wangu mwelekevu Antipa alipouawa huko kwenu, Satani anakokaa. Lakini ninayokuonya, ni machache, ya kuwa unao kwako wanaoushika ufundisho wa Bileamu aliyemfundisha Balaka kukwaza wana wa Isiraeli, akiwafundisha kula nyama za tambiko na kufanya ugoni. Vivyo hivyo hata wewe unao wanaoyashika mafundisho ya Wanikolai yaliyo hivyo. Sasa juta! Usipojuta, nitakujia upesi, nipigane nao kwa upanga uliomo kinywani mwangu. Mwenye masikio na asikie, Roho anavyowaambia wateule! Mwenye kushinda nitamgawia ile Mana iliyofichwa, kisha nitampa kijiwe cheupe, namo katika kijiwe hiki limeandikwa jina jipya lisilojulika kwa mtu, asipokuwa mwenye kulipata. Malaika wa wateule walioko Tiatira mwandikie: Ndivyo, anavyosema Mwana wa Mungu aliye mwenye macho yaliyo kama moto unaowaka, ambaye miguu yake imefanana na shaba nyekundu: Nayajua matendo yako ya kupenda na ya kumtegemea Mungu na ya kutumikia na ya kuvumilia kwako. Tena najua: kazi zako za mwisho ni nyingi kuliko za kwanza. Lakini ninakuonya, ya kuwa humkatai mwanamke Izebeli anayejisema kuwa mfumbuaji, akiwafundisha na kuwapoteza watumwa wangu, wafanye ugoni, tena wale nyama za tambiko. Nimempa siku za kujuta, lakini hataki kujuta na kuuacha ugoni wake. Tazama, nitambwaga kitandani, nao waliofanya naye ugoni vilevile, waumizwe sana, wasipojuta na kuyaacha matendo yake. Hata watoto wake nitawaua, wafe. Ndipo, wateule wote watakaponitambua, ya kuwa mimi ni mwenye kuyapeleleza mafigo, hata mioyo. Nami nitawapa ninyi kila mmoja, kama matendo yenu yalivyo. Wengine wenu ninyi, mlioko Tiatira, msioyafuata hayo mafundisho, msiovitambua vilindi vya Satani, nawaambia ninyi kwa mfano: Siwatwiki mzigo wa wengine, ila hicho, mlicho nacho, kishikeni, mpaka nitakapokuja! Mwenye kushinda na kuzishika kazi zangu mpaka mwisho nitampa kuwa mkuu wa wamizimu; naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, awapondeponde kama vyungu vya udongo. Kama nami nilivyopewa na Baba yangu, nitampa naye nyota ya mapema. Mwenye masikio na asikie, Roho anayowaambia wateule! Malaika wa wateule walioko Sarde mwandikie: Ndivyo anavyosema yeye aliye mwenye zile roho saba za Mungu na mwenye zile nyota saba. Nayajua matendo yako, unalo jina la kuwa unaishi, lakini u mfu. Amka, uyashupaze masao yanayotaka kufa nayo! Kwani sikuyaona matendo yako, ya kuwa yametimilika mbele ya Mungu wangu. Kumbuka, uliyoyapokea! Nayo uliyoyasikia, yashike, upate kujuta! Usipokesha, nitakuja kama mwizi, usiitambue saa, nitakayokujia wewe. Lakini unayo majina machache huko Sarde wasiozichafua nguo zao. Ndio watakaoenenda pamoja nami wenye nguo nyeupe, kwani zimewapasa. Mwenye kushinda atavikwa naye nguo nyeupe, nalo jina lake sitalifuta katika kitabu cha uzima. Nami nitaliungama jina lake mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika zake. Mwenye masikio na asikie, Roho anayowaambia wateule! Malaika wa wateule walioko Filadelfia mwandikie: Ndivyo, anavyosema yeye Mtakatifu aliye mwenye kweli, aliye hata mwenye ufunguo wa Dawidi. Atakapofungua, hatakuwako awezaye kupafunga tena; atakapofunga, hatakuwako awezaye kupafungua. Nayajua matendo yako, tazama mbele yako nimekupa mlango ulio wazi, tena hakuna awezaye kuufunga. Kweli nguvu, ulizo nazo, ni ndogo, lakini umelishika Neno langu, hukulikana Jina langu. Tazama, nitakupa wanafunzi wa Satani wanaojisema kuwa Wayuda, lakini sio, ila husema uwongo. Tazama, nitawaleta hao, waje, wakuangukie penye miguu yako, watambue, ya kuwa mimi nimekupenda wewe. Kwa sababu umelishika Neno langu la uvumilivu, nitakulinda nami, nikuokoe katika saa ya majaribu itakayopafikia pote panapokaa watu kwamba: Wakaao nchini wajaribiwe. Ninakuja upesi. Shikamana nayo, uliyo nayo, mtu asikitwae kilemba chako! Mwenye kushinda nitamfanya kuwa nguzo Jumbani mwa Mungu wangu, asitoke tena nje. Nami nitamwandika Jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, la Yerusalemu mpya, utakaoshuka toka mbinguni kwake Mungu wangu. Nitamwandika hata Jina langu jipya. Mwenye masikio na asikie, Roho anayowaambia wateule! Malaika wa wateule walioko Laodikia mwandikie: Ndivyo, anavyosema yeye Amin aliye shahidi mwelekevu na mkweli, aliye wa kwanza wa viumbe vyote vya Mungu. Nayajua matendo yako, wewe huzizimiki, wala huzizimuki. Ungefaa ukiwa mwenye kuzizimika au mwenye kuzizimuka. Lakini sasa, kwa kuwa u mwenye kuvuvuwaa, usiwe mwenye kuzizimika wala mwenye kuzizimuka, nitakutema kinywani mwangu. Kwani unasema: Mimi niko na mali, ninayo malimbiko yangu, hakuna, nilichokikosa. Nawe hujui, ya kuwa wewe u mnyonge, unapaswa na kugawiwa, u maskini na kipofu na mwenye uchi. Nakuonyesha mzungu, ndio huu: nunua kwangu dhahabu iliyong'azwa na moto, upate kuwa mwenye mali! Nunua nazo nguo nyeupe, upate kuvaa, uchi wako usionekane, ukakutia soni! Nunua nayo mafuta ya macho, uyapake macho yako, upate kuona! Wote, ninaowapenda mimi, nawaonya na kuwapiga. Kwa hiyo jikaze, ujute! Tazama, nimesimama mlangoni nikipiga hodi. Mtu atakayenisikia sauti yangu, akaufungua mlango, basi, nitaingia mwake, nile pamoja naye, naye ale pamoja nami. Mwenye kushinda nitampa kukaa pamoja nami kitini pangu pa kifalme, kama mimi nami nilivyoshinda, nikakaa pamoja na Baba yangu kitini pake pa kifalme. Mwenye masikio na asikie, Roho anayowaambia wateule! Kisha nalitazama, nikaona mlango mbinguni uliokuwa wazi. Ndipo, sauti ile ya kwanza, niliyoisikia kama ya baragumu, iliyosema nami, iliposema: Panda huku, nikuonyeshe yatakayofanyika, haya yakiisha! Papo hapo nikawapo kiroho. Nikaona kiti cha kifalme, kilikuwa kimewekwa mbinguni; humo kitini mlikuwamo mwenye kukikalia. Huyu aliyekaa, ukimtazama, alifanana na kijiwe cha yaspi na cha sardio; hata upindi wa Mungu ulikizunguka kiti, kwa kuutazama, ulifanana na kijiwe cha sumaradi. Tena viti 24 vya kifalme vilikizunguka kiti kile; nikaona wazee 24 waliokaa mle vitini, waliokuwa wamevaa nguo nyeupe na vilemba vya dhahabu vichwani pao. Hapo penye kiti cha kifalme palipiga umeme na vivumo na ngurumo, tena palikuwa na mienge saba ya moto iliyowaka mbele ya kiti cha kifalme, ndio zile roho saba za Mungu. Tena mbele ya kiti cha kifalme kulikuwako yenye mfano wa bahari ya kioo iliyofanana na ulanga uangazikao. Napo katikati penye kiti cha kifalme na kukizunguka kiti cha kifalme palikuwa na nyama wanne waliojaa macho mbele na nyuma. Nyama wa kwanza alifanana na simba, nyama wa pili alifanana na dume la ng'ombe, nyama wa tatu alikuwa na uso kama wa kimtu, nyama wa nne alifanana na tai mwenye kuruka. Kila mmoja wao hao nyama wanne alikuwa na mabawa sita yaliyojaa macho po pote, nje ndani; hawapumziki mchana wala usiku wakisema: Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Bwana Mungu, yeye Mwenyezi aliyekuwapo, aliopo, atakayekuja. Hao nyama walipomtukuza na kumheshimu na kumshukuru yule aliyekaa kitini mwa kifalme, aliye mwenye kuwapo kale na kale pasipo mwisho, ndipo, wale wazee 24 walipomwangukia yule aliyekaa kitini mwa kifalme na kumtambikia yeye aliye mwenye kuwapo kale na kale pasipo mwisho; wakavitupa vilemba vyao mbele ya kiti cha kifalme wakisema: Wewe Bwana na Mungu wetu, umepaswa na kupewa utukufu na heshima na uwezo, kwani wewe uliviumba vyote; kwa hayo, uyatakayo, vikapata kuwapo vilipokwisha kuumbwa. Nikaona mkononi mwa kuume mwake yule aliyekaa kitini mwa kifalme kitabu kilichoandikwa ndani na mgongoni, nacho kilikuwa kimetiwa muhuri saba. Kisha nikaona malaika mwenye nguvu, akatangaza kwa sauti kuu: Yuko nani apaswaye na kukifungua kitabu na kuziondoa muhuri zake? Hakuwako hata mmoja wala mbinguni wala nchini wala kuzimuni aliyeweza kukifungua kitabu na kukitazama. Ndipo, nilipolia sana, kwa sababu hakuonekana hata mmoja apaswaye na kukifungua kitabu na kukitazama. Mmoja wao wale wazee akaniambia: Usilie! Tazama, yule simba wa shina la Yuda aliye mzizi wa Dawidi, yeye ameshinda, apate kukifungua kitabu na kuziondoa muhuri zake saba. Kisha nikaona mwana kondoo aliyesimama katikati penye kiti cha kifalme na wale nyama wanne na wale wazee, naye alikuwa, kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba; ndio zile roho saba za Mungu zilizotumwa kwenda kuzifikia nchi zote. Alipokuja akakitwaa kitabu mkononi mwa kuume mwake yeye aliyekaa kitini mwa kifalme. Hapo alipokitwaa kitabu, ndipo, wale nyama wanne na wale wazee 24 walipomwangukia Mwana kondoo. Wakawa wameshika kila mmoja zeze na vyano vya dhahabu vilivyojaa uvumba, ndio maombo ya watakatifu. Nao wakaimba wimbo mpya wakisema: Wewe umepaswa na kukipokea kitabu na kuziondoa muhuri zake, kwani umechinjwa, umkombolee Mungu kwa damu yako watu wa mashina yote na wa misemo yote na wa makabila yote na wa wamizimu wote, ukawafanya, wawe wafalme na watambikaji wa Mungu wetu; ndio watakaozitawala nchi. Kisha nikaona, nikasikia sauti ya malaika wengi waliokizunguka kiti cha kifalme na wale nyama na wale wazee. Nilipowahesabu, walikuwa maelfu na maelfu na maelfu, wakasema kwa sauti kuu: Mwana kondoo aliyechinjwa amepaswa na kupokea uwezo na malimbiko na werevu wa kweli na nguvu na heshima na utukufu na mapongezo. Navyo viumbe vyote vilivyoko mbinguni, navyo vilivyopo nchini, navyo vilivyoko kuzimuni, navyo vilivyomo baharini, navyo vyote vilivyomo ndani yao, nikavisikia, vikisema: Mpeni yeye aliyekaa kitini mwa kifalme naye Mwana kondoo mapongezo na heshima na utukufu na nguvu kale na kale pasipo mwisho! Wale nyama wanne waliposema: Amin, ndipo, wale wazee walipoanguka chini, wakamsujudia mwenye kuishi kale na kale. Kisha nikamwona Mwana kondoo, akifungua moja ya zile muhuri saba. Nikasikia, mmoja wa wale nyama wanne akisema kama kwa sauti ya ngurumo: Njoo! Nikatazama, nikaona farasi mweupe, naye aliyempanda alikuwa na uta, akapewa kilemba; kisha yeye aliyekuwa mshindaji akatoka, ashinde tena. Alipoifungua muhuri ya pili, nikasikia, nyama wa pili akisema: Njoo! Pakatokea farasi mwingine, ni mwekundu sana; aliyempanda akapewa kuuondoa utengemano katika nchi, wapate kuuana wao kwa wao. Naye akapewa upanga mkubwa. Alipoifungua muhuri ya tatu, nikasikia, nyama wa tatu akisema: Njoo! Nikatazama, nikaona farasi mweusi, naye aliyempanda alikuwa na kipimo mkononi mwake. Nikasikia iliyokuwa kama sauti iliyokuwa katikati ya wale nyama wanne, ikisema: Kibaba cha mchele ni shilingi, vibaba vitatu vya mtama ni shilingi. Lakini mafuta usiyapotoe, wala mvinyo! Alipoifungua muhuri ya nne, nikasikia, nyama wa nne akisema: Njoo! Nikatazama, nikaona farasi wa kijivujivu, naye aliyempanda jina lake Kifo, nao wazimu wakafuatana naye. Wakapewa nguvu ya fungu la nne la nchi, wawaue kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa yauayo na kwa nyama wakali waliopo nchini. Alipoifungua muhuri ya tano, nikaona, mvunguni mwa meza ya Bwana zimo roho zao waliouawa kwa ajili ya Neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda, walioushuhudia. Nao wakalia kwa sauti kuu wakisema: Mpaka lini, wewe Bwana uliye mtakatifu na mkweli? Mbona huwahukumu wanaokaa nchini, uzilipize damu zetu? Ndipo, walipopewa kila mmoja kanzu nyeupe, wakaambiwa, wanyamaze siku chache tena, mpaka yatimilike mambo ya watumwa wenzao nayo ya ndugu zao watakaouawa vivyo hivyo kama wao wenyewe. Nikamwona, alipoifungua muhuri ya sita. Pakawa tetemeko kubwa la nchi, hata jua likawa jeusi kama gunia la makonge, mwezi wote ukawa kama damu, nyota za mbinguni zikaanguka nchini, kama mkuyu unavyoyabwaga mapooza yake ukitikiswa na upepo mwingi. Kisha mbingu zikatengeka kama karatasi linalojizinga upesi, hata milima yote na visiwa vyote vikaondolewa mahali pao. Ndipo, wafalme wa nchini, nao walio wakubwa, nao wakuu wa vikosi, nao wenye mali, nao wenye nguvu, nao watumwa wote, nao waungwana wote walipojificha mapangoni na miambani penye milima wakiiambia milima na miamba: Tuangukieni, mtufiche machoni pake yeye anayekaa kitini mwa kifalme napo penye makali ya Mwana kondoo! Kwani imekuja siku kubwa ya makali yao, yuko nani awezaye kusimama? Kisha nikaona malaika wanne waliosimama penye pembe nne za nchi, wakizishika pepo nne za nchi, maana upepo usivume nchini wala baharini wala penye mti wo wote. Nikaona malaika mwingine aliyepanda toka maawioni kwa jua, alikuwa na muhuri ya Mungu aliye Mwenye uzima, akawaita kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuzipotoa nchi na bahari, akasema: Msizipotoe nchi wala bahari wala miti, mpaka tuishe kuwatia watumwa wa Mungu wetu muhuri penye mapaji yao. Ndipo, nilipoisikia hesabu yao waliotiwa muhuri, walikuwa 144000 wenye kutiwa muhuri ya mashina yote ya wana wa Isiraeli: Waliotiwa muhuri ya shina la Yuda walikuwa 12000, muhuri ya shina la Rubeni walikuwa 12000, muhuri ya shina la Gadi walikuwa 12000, muhuri ya shina la Aseri walikuwa 12000, muhuri ya shina la Nafutali walikuwa 12000, muhuri ya shina la Manase walikuwa 12000, muhuri ya shina la Simeoni walikuwa 12000, muhuri ya shina la Lawi walikuwa 12000, muhuri ya shina la Isakari walikuwa 12000, muhuri ya shina la Zebuluni walikuwa 12000, muhuri ya shina la Yosefu walikuwa 12000, muhuri ya shina la Benyamini walikuwa 12000, *Kisha nikatazama, nikaona mkutano mwingi usiohesabika na mtu wo wote, ni watu wa wamizimu wote na wa mashina yote na wa makabila yote na wa misemo yote. Walisimama mbele ya kiti cha kifalme na mbele ya Mwana kondoo; walikuwa wamevikwa kanzu nyeupe, namo mikononi mwao walishika makuti ya mitende. Nao wakatoa sauti kuu wakisema: Wokovu ni wa Mungu wetu akaaye kitini mwa kifalme na wa Mwana kondoo! Ndipo, malaika wote waliosimama na kukizunguka kiti cha kifalme na wale wazee na wale nyama wanne, walipoanguka nyusoni pao mbele ya kiti cha kifalme, wakamsujudia Mungu wakisema: Kweli, mapongezo na utukufu na werevu wa kweli na shukrani na heshima na uwezo na nguvu ni za Mungu wetu kale na kale pasipo mwisho! Amin. Mmoja wao wale wazee akaniuliza akisema: Hawa waliovikwa kanzu nyeupe ni akina nani? Nao wametoka wapi? Nikamwambia: Bwana wangu, wewe unajua. Akaniambia: Hawa ndio waliotoka katika maumivu makubwa, ndio waliozifua nguo zao na kuzing'aza kwa damu ya Mwana kondoo. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha kifalme cha Mungu na kumtumikia mchana na usiku Jumbani mwake. Anayekaa kitini mwa kifalme atakapotua kwao, hawataona tena njaa wala kiu, wala jua halitawachoma wala jasho lo lote. Kwani Mwana kondoo aliomo katikati ya kiti cha kifalme atawachunga na kuwaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.* Alipoifungua muhuri ya saba, vyote vilivyomo mbinguni vikawa kimya kama nusu saa. Nikawaona wale malaika saba waliosimama mbele ya Mungu, wakipewa mabaragumu saba. Kisha akaja malaika mwingine, akasimama mbele ya meza ya Bwana; huyu alikuwa na chetezo cha dhahabu cha kuvukizia. Akapewa uvumba mwingi, auvukize juu ya meza ya Bwana iliyo ya dhahabu, iliyoko mbele ya kiti cha kifalme, watakatifu wote watakapoomba. Moshi wa uvumba ulipopanda kutoka mkononi mwa huyo malaika pamoja na maombo ya watakatifu, ukamfikia Mungu. Kisha malaika akakitwaa kile chetezo cha kuvukizia, akakijaza moto uliokuwako juu ya meza ya Bwana, akakibwaga nchini. Kukawa na ngurumo na uvumi na umeme na tetemeko la nchi. Ndipo, wale malaika saba waliokuwa na yale mabaragumu saba walipojiweka tayari kuyapiga. Wa kwanza alipopiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na ya moto iliyochanganyika na damu, ikabwagwa nchini. Pakateketea fungu la tatu la nchi, hata fungu la tatu la miti likateketea, hata majani mabichi yote yakateketea. Malaika wa pili alipopiga baragumu, pakatupwa baharini yaliyokuwa kama mlima mkubwa uliowaka moto. Ndipo, fungu la tatu la bahari lilipokuwa damu; hata fungu la tatu la viumbe vya baharini vilivyokuwa vyenye uzima vikafa, hata fungu la tatu la vyombo vikaangamia. Malaika wa tatu alipopiga baragumu, pakaanguka toka mbinguni nyota kubwa iliyowaka moto kama wa mwenge, ikaanguka penye fungu la tatu la mito na la chemchemi za maji. Nyota hiyo jina lake huitwa Abisinto. Ndipo, fungu la tatu la maji lilipokuwa na uchungu sana. Watu wengi wakafa kwa yale maji, kwa sababu yalikuwa yenye uchungu uuao. Malaika wa nne alipopiga baragumu, pakapigwa fungu la tatu la jua na fungu la tatu la mwezi na fungu la tatu la nyota; hayo mafungu yao ya tatu yakawa yenye giza, yasiangaze mchana wala usiku vilevile. Nikaona, nikasikia, tai mmoja aliyeruka mbinguni kati akisema kwa sauti kuu: Kondo! Kondo! Kondo! Zitawapata wakaao katika nchi, yatakapolia mabaragumu yaliyosalia ya wale malaika watatu waendao kuyapiga! Malaika wa tano alipopiga baragumu, nikaona nyota iliyokuwa imetoka mbinguni, ikaanguka nchini. Kisha ikapewa ufunguo wa kisima cha kuzimu, ikakifungua hicho kisima cha kuzimu. Ndipo, ulipopanda moshi kutoka mle kisimani kama moshi wa jiko kubwa. Jua likatiwa giza, hata anga vilevile kwa ajili ya moshi huo wa kisimani. Mle katika moshi mkatoka nzige, wakazifunika nchi, wakapewa nguvu, kama nge wa nchi walivyo na nguvu. Wakaambiwa, wasiyapotoe majani ya nchi wala cho chote kilicho kibichi, wala miti yo yote, ila wawapotoe watu tu wasio na muhuri ya Mungu mapajani. Hawakupewa kuwaua, ila walipewa, wawaumize tu miezi mitano. Maumivu hayo yalikuwa kama maumivu ya nge, akimwuma mtu. Siku zile watu watakutafuta kufa, wasikuone; watakutunukia kufa, lakini kufa kutawakimbia. Umbo la nzige hao lilikuwa limefanana kama la farasi walio tayari kupiga vita. Vichwani pao hapo juu palikuwa kama vilemba vilivyofanana na dhahabu. Nyuso zao lilikuwa kama nyuso za watu. Nywele, walizokuwa nazo, zilikuwa kama nywele za wanawake, nayo meno yao yalikuwa kama meno ya simba. Vifuani walikuwa na ngao kama ngao za vyuma. Uvumi wa mabawa yao ulikuwa kama uvumi wa magari yavutwayo mbiombio na farasi wengi kwenda vitani. Walikuwa wenye mikia kama ya nge yenye machomeo; namo mikiani mwao ndimo, nguvu zao zilimokuwa za kuwapotoa watu miezi mitano. Wana mfalme wao, ni malaika wa kuzimu, jina lake Kiebureo huitwa Abadoni, Kigiriki huitwa Apoloni. Pigo la kwanza limekwisha pita; tazama, yako bado mawili, yanakuja baadaye. Malaika wa sita alipopiga baragumu, nikasikia sauti moja iliyotoka katika zile pembe nne za meza ya Bwana ya dhahabu iliyokuwako mbele ya Mungu, ikamwambia yule malaika wa sita aliyekuwa na baragumu: Wafungue wale makaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa wa Eufurati. Ndipo, walipofunguliwa wale malaika wanne waliokuwa wamewekewa saa hii ya siku hii ya mwezi huu wa mwaka huu, waliue fungu la tatu la watu. Hesabu ya vikosi vya wapanda farasi ilikuwa elfu ishirini mara elfu kumi (20000000); ndiyo hesabu yao, niliyoisikia. Nilipowatazama wale farasi nao waliowapanda, nikawaona kuwa hivyo: walikuwa wamevaa nguo za vyuma kama za moto, nyingine nyeusi, nyingine za manjano. Vichwa vya farasi vilikuwa kama vya simba, tena katika vinywa vyao hutoka moto na moshi na viberitiberiti. Fungu la tatu la watu likauawa kwa mapigo hayo matatu, kwa moto na kwa moshi na kwa viberitiberiti vilivyotoka vinywani mwao. Kwani nguvu za hao farasi zimo vinywani mwao namo mikiani mwao. Kwani mikia yao imefanana na nyoka wenye vichwa; hiyo ndiyo, waliyopotoa nayo. Watu waliosalia, wasiouawa na mapigo hayo, hawakuyajutia matendo ya mikono yao, maana hawakuacha kutambikia mizimu na vinyago vya dhahabu na vya fedha na vya shaba na vya mawe na vya miti visivyoweza kuona wala kusikia wala kwenda. Kwa hiyo hawakujutia wala uuaji wao wala uchawi wao wala ugoni wao wala wizi wao. Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu aliyeshuka toka mbinguni; vazi lake lilikuwa wingu, kofia la kichwani pake lilikuwa upindi wa Mungu, uso wake ulikuwa kama jua, miguu yake ilikuwa kama nguzo zenye moto. Mkononi mwake alishika kitabu kidogo kilichokuwa kimefunuka. Mguu wake wa kuume ulikanyaga juu ya bahari, wa kushoto juu ya nchi. Akapaza sauti kuu, kama simba anavyolia. Naye alipopaza sauti, ngurumo saba zilizitoa sauti zao. Hizo ngurumo saba zilipokwisha sema, nalitaka kuandika. Ndipo, niliposikia sauti toka mbinguni, ikisema: Yafiche na kuyatia muhuri, hizo ngurumo saba ziliyoyasema, lakini usiyaandike! Naye malaika, niliyemwona, alivyosimama mguu mmoja baharini na mmoja nchini, akauelekeza mkono wake wa kuume mbinguni, akaapa na kumtaja yeye aliye Mwenye uzima kale na kale pasipo mwisho, aliyeziumba mbingu navyo vilivyomo ndani yake, hata nchi navyo vilivyomo ndani yake, hata bahari navyo vilivyomo ndani yake, akisema: Hapatakuwa siku tena, ila siku ya sauti ya malaika wa saba, atakapopiga baragumu, ndipo, patakapotimia fumbo la Mungu, kama alivyowapigia mbiu njema wale wafumbuaji waliokuwa watumwa wake. Ndipo, ile sauti, niliyoisikia toka mbinguni, iliposema tena nami kwamba: Nenda, ukitwae kile kitabu kidogo kilichokuwa kimefunuka, kilichomo mkononi mwa malaika aliyesimama mguu mmoja baharini na mmoja nchini! Nikaenda kwa yule malaika, nikamwambia, anipe kile kitabu kidogo. Naye akaniambia: Kitwae, kile! Kitakutia uchungu tumboni mwako, lakini kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali. Nikakitwaa kile kitabu kidogo mkononi mwa yule malaika, nikakimeza, nacho kilikuwa kitamu kama asali kinywani mwangu; lakini nilipokwisha kukimeza nikatiwa uchungu tumboni mwangu. Wakaniambia: Wewe imekupasa kufumbulia tena makabila mengi na wamizimu wengi na wenye misemo mingi na wafalme wengi. Kisha nikapewa mwanzi uliofanana na fimbo, nikaambiwa: Inuka, ulipime Jumba la Mungu na meza ya Bwana nao wenye kutambikia mlemle! Lakini ua ulioko nje penye Jumba la Mungu uuache nje, usiupime! Kwani huo wamizimu wamepewa, waukanyage mji mtakatifu miezi 42. Nami nitawapa mashahidi wangu wawili, wawafumbulie siku 1260 wakiwa wamevaa magunia. Hao ndio ile michekele miwili na ile mienge miwili iliyosimama mbele ya Bwana wa nchi. Tena mtu akitaka kuwapotoa, hutoka moto vinywani mwao na kuwala hao wachukivu wao. Kila atakaye kuwapotoa sharti auawe hivyo. Hao wanazo nguvu za kuzifunga mbingu, mvua isinye siku za ufumbuaji wao. Tena wanazo nguvu za maji za kuyageuza kuwa damu na za kuipiga nchi mapigo yo yote napo po pote, watakapotaka. Nao watakapoumalizia ushahidi wao, patatoka nyama mkali kuzimuni, atafanya vita nao, mpaka awashinde, awaue. Kisha mizoga yao itakaa katika njia ya mji ule mkubwa unaoitwa kiroho Sodomu na Misri; ndipo, naye Bwana wao alipowambwa msalabani. Nao watu wa makabila na wa mashina na wa misemo na wa wamizimu wataiona mizoga yao siku tatu na nusu, lakini hawataacha, mizoga yao izikwe kaburini. Kwa hiyo wakaao nchini watashangilia kwa ajili yao na kupiga vigelegele na kupelekeana matunzo, kwa sababu wafumbuaji wale wawili waliwatesa wakaao nchini. Lakini siku tatu na nusu zilipopita, roho ya uzima ilitoka kwa Mungu, ikawaingia; ndipo, waliposimama kwa miguu yao, woga mwingi ukawaguia waliowaona. Kisha wakasikia sauti kuu toka mbinguni iliyowaambia: Pandeni huku! Walipopanda mbinguni katika wingu, wachukivu wao walikuwa wanawatazama. Saa ileile pakawa tetemeko kubwa la nchi, nalo fungu la kumi la mji likafudikizwa, watu waliouawa na hilo tetemeko la nchi majina yao yalikuwa 7000. Nao waliosalia wakashikwa na woga, wakamtukuza Mungu wa mbingu. Pigo la pili limekwisha kupita. Tazama, la tatu linakuja upesi. Malaika wa saba alipopiga baragumu, kukawa na sauti kuu nyingi mbinguni zikisema: Ufalme wa ulimwengu umekwisha kuwa wake Bwana wetu na wa Kristo wake; ndiye atakayetawala kale na kale pasipo mwisho. Ndipo, wale wazee 24 waliokaa mbele ya Mungu katika viti vyao vya kifalme walipoanguka nyusoni pao, wakamsujudia Mungu na kusema: Twayavumisha mema yako wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, Ndiwe aliopo naye aliyekuwapo! Umekwisha kuutwaa ufalme kwa uwezo wako mwingi. Wamizimu walipopatwa na makali ndipo, makali, yako yalipotokea, ndipo, siku yako ilipotimia ya kuwahukumu wafu na ya kuwapokeza watumwa wako walio wafumbuaji nao watakatifu nao walioliogopa Jina lako, walio wadogo nao walio wakubwa. Siku imetimia ya kuwaangamiza wenye kuiangamiza nchi. Kisha Jumba la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, mkaonekana mlemle Jumbani mwa Mungu Sanduku la Agano lake. Kukapiga umeme na uvumi na ngurumo, kukawa na tetemeko la nchi na mvua nyingi sana ya mawe. Kisha kukaonekana kielekezo kikubwa mbinguni: mwanamke aliyekuwa amevikwa jua alikuwa anao mwezi chini miguuni pake, napo kichwani pake alikuwa na kilemba cha nyota kumi na mbili. Kwa kuwa ana mimba, akalia kwa kuona uchungu na maumivu ya kuzaa. Kisha kukaonekana kielekezo kingine mbinguni, ni joka kubwa lililo jekundu kama moto; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, tena vichwani pake alikuwa mwenye vilemba saba vya kifalme. Mkia wake ulikokota fungu la tatu la nyota za mbinguni, ukazibwaga nchini. Kisha huyo joka akaja kusimama mbele ya yule mwanamke aliyetaka kuzaa, kusudi hapo, atakapozaa, ammeze mtoto wake. Ndivyo, alivyozaa mwana wa kiume atakayewachunga wamizimu wote kwa fimbo ya chuma. Huyu mtoto wake akapokonywa, akapelekwa kwake Mungu penye kiti chake cha kifalme, naye mwanamke akakimbilia nyikani, alipokuwa na mahali, alipotengenezewa na Mungu, wamlishe hapo siku 1260. Kukawa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakaja kupigana na yule joka; yule joka na malaika zake walipopiga vita, hawakushinda, tena hapakuonekana mahali pao pa kukaa mbinguni. Kisha yule joka kubwa akabwagwa nchini, ni yule nyoka wa kale aitwaye Msengenyaji na Satani aliyeupoteza ulimwengu wote, akabwagwa nchini, nao malaika zake wakabwagwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema: Sasa wokovu na uwezo na ufalme umekuwa wa Mungu wetu, nazo nguvu zimekuwa zake Kristo wake, kwani msutaji wa ndugu zetu amebwagwa nchini; ndiye aliyewasuta mbele ya Mungu wetu mchana na usiku. Nao wamemshinda kwa nguvu ya damu ya Mwana kondoo na kwa nguvu ya neno la ushahidi wao. Nao hawakujipenda wenyewe mpaka kufa. Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu nanyi mkaao mwake! Lakini ninyi nchi na bahari, yatawapata! Kwani Msengenyaji ameshuka kwenu ninyi mwenye makali mengi moyoni, kwani ajua, ya kuwa siku zake ni chache tu. Yule joka alipoona, ya kuwa amebwagwa nchini, ndipo, alipomkimbiza yule mwanamke aliyemzaa yule mtoto wa kiume. Lakini mwanamke akapewa mabawa mawili ya yule tai mkibwa, aende nyikani na kuruka, apafikie mahali pake, anapolishwa siku hizi nazo zitakazokuja nacho kipande cha siku zitakazosalia, atoke usoni pake yule joka. Ndipo, yule joka alipotoa maji kinywani mwake kama mto, akamtemea yule mwanamke kwamba amtose mle mtoni. Lakini nchi ikamsaidia yule mwanamke, maana hiyo nchi ikakifumbua kinywa chake, ikaunywa ule mto, yule joka alioutoa kinywani mwake. Kwa hiyo yule joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake kufanya vita nao waliosalia wa uzao wake, ndio wale walioyashika maagizo yake Mungu, waliofuliza kumshuhudia Yesu. Kisha nikapelekwa kusimama ufukoni penye bahari. Nikaona nyama mkali, akitoka baharini mwenye pembe kumi na vichwa saba; juu hizo pembe zake zilikuwa na vilemba kumi vya kifalme, napo vichwani pake palikuwa na majina ya kumtukana Mungu. Huyu nyama, niliyemwona, alifanana na chui, lakini miguu yake ilikuwa kama ya nyegere; nacho kinywa chake kilikuwa kama kinywa cha simba. Yule joka akampa uwezo wake na kiti chake cha kifalme na nguvu nyingi. Miongoni mwa vichwa vyake nikaona kimoja kilichokuwa, kama kimepasuliwa kwa kuuawa, lakini donda lake la kuuawa lilikuwa limepona. Ulimwengu wote ukamtazama yule nyama na kumstuka, kisha wakamwangukia yule joka, kwa sababu alimpa yule nyama nguvu zake, wakamwangukia naye yule nyama wakisema: Yuko nani anayefanana na nyama huyu? Tena yuko nani anayeweza kupiga vita naye? Kisha akapewa domo la kusema makuu ya kumtukana Mungu, akapewa nguvu ya kuyafanya hayo mambo yake miezi 42. Ndipo, alipolifunua domo lake, amtukane Mungu, alitukane nalo Jina lake na tuo lake nao wakaao mbinguni. Tena akapewa kufanya vita nao watakatifu na kuwashinda, akapewa nguvu ya kushinda hata mashina na makabila na misemo na wamizimu wote. Kwa hiyo watamwangukia yeye wote wakaao nchini, ambao tangu hapo, ulimwengu ulipoumbwa, hawakuandikwa majina yao katika kitabu cha uzima cha Mwana kondoo aliyechinjwa. Mtu akiwa na masikio na asikie! Kama yuko mwenye kuteka, naye atatekwa; kama yuko mwenye kuua kwa upanga, naye sharti auawe kwa upanga. Hapo ndipo, watakatifu watakapovumilia kwa kumtegemea Mungu. Nikaona nyama mwingine, akitoka katika nchi; huyu alikuwa na pembe mbili kama mwana kondoo, akasema kama joka. Hata nguvu zote za yule nyama wa kwanza aliyemtangulia huzitumia, aishurutishe nchi nao wakaao nchini, wamwangukie yule nyama wa kwanza aliyepona donda lake la kuuawa. Hufanya vielekezo vikubwa, hata kushusha moto toka mbinguni, uanguke nchini machoni pa watu. Kwa hivyo vielekezo, alivyopewa kuvifanya mbele ya yule nyama, huwadanganya wakaao nchini akiwaambia wale wakaao nchini, wafanye kinyago cha mfano wa yule nyama aliyekuwa na kidonda cha upanga, akapata kupona. Kisha akapewa kukitia pumzi kinyago cha yule nyama, hicho kinyago cha yule nyama kiseme; kwa hiyo nguvu yake wakauawa wote wasiokiangukia kinyago hicho cha yule nyama. Kwani anawashurutisha wote, wadogo na wakubwa, wenye mali na wakosao mali, waungwana na watumwa, wajitie chapa mikononi mwao mwa kuume au mapajini pao, maana mtu asiweze kununua au kuuza kitu, asipokuwa na chapa cha jina la yule nyama au kiwango cha jina lake. Hapa ndipo panapotakwa werevu wa kweli; aliye mwenye akili na akifumbue kiwango cha yule nyama! Nacho kiwango chake ndicho mia sita na sitini na sita (666). Kisha nikamwona Mwana kondoo, akisimama mlimani kwa Sioni juu. Pamoja naye kulikuwako watu 144000 waliokuwa wameandikwa Jina lake na Jina la Baba yake mapajini pao. Nikasikia sauti toka mbinguni kama uvumi wa maji mengi na kama uvumi wa ngurumo kuu. Hizo sauti, nilizozisikia, zilikuwa kama za wapiga mazeze, wakiyapiga mazeze yao. Wakaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha kifalme penye wale nyama wanne na wale wazee. Hakuwako mtu aliyeweza kujifunza ule wimbo, wasipokuwa wale 144000 waliokombolewa na kuondolewa nchini. Hawa ndio wasiochafuliwa na wanawake; kwa hiyo huwa kama vijana. Tena ndio wamfuatao Mwana kondoo po pote, anapokwenda, kwa kuwa walikombolewa kwenye watu, wawe malimbuko yake Mungu nayo yake Mwana kondoo. Vinywani mwao hamkuonekana uwongo; wako pasipo kilema. Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka mbinguni kati na kuushika Utume mwema wa kale na kale wa kuwatangazia nchini wamizimu wote na mashina yote na misemo yote na makabila yote. Naye akasema kwa sauti kuu: Mcheni Mungu na kumtukuza! Kwani saa ya hukumu yake imekuja. Mwangukieni yeye aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji! Pakafuata mwingine, ni malaika wa pili, akasema: Umeanguka! Umeanguka mji mkubwa wa Babeli uliowanywesha wamizimu wote mvinyo ya ugoni wake itokezayo makali. Pakawafuata mwingine, ni malaika wa tatu, akasema kwa sauti kuu: Mtu akimwangukia yule nyama na kinyago chake na kujitia chapa chake pajini pake au mkononi pake, huyo atakunywa mvinyo yenye makali ya Mungu, iliyoandaliwa pasipo kuchanganywa na maji katika kinyweo cha makali yake, kisha ataumizwa motoni mwenye viberitiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwana kondoo. Moshi wa maumivu yao hupanda kale na kale, hawapati mapumziko mchana na usiku hao waliomwangukia yule nyama na kinyago chake, nao waliojitia chapa cha jina lake. Hapa ndipo, watakatifu watakapovumilia, wayashikao maagizo ya Mungu wakifuliza kumtegemea Yesu. Kisha nikasikia sauti toka mbinguni, ikisema: Andika: Wenye shangwe ni wafu waliokufa na kumtegemea Bwana tangu sasa. Kweli Roho anasema: Huyapumzikia masumbuko yao, kwani matendo yao hufuatana nao. Nilipotazama tena nikaona wingu jeupe, humo winguni juu palikaa aliyefanana na mwana wa mtu; alikuwa na kilemba cha dhahabu kichwani pake, mkononi mwake alishika mndu mkali. Hapo akatoka malaika mwingine Jumbani mwa Mungu, akapiga sauti kuu ya kumwambia yule aliyekaa winguni juu kwamba: Tuma mndu wako, uvune! Kwani saa ya kuvuna imekuja, kwa kuwa mavuno yaliyoko nchini yamekauka. Ndipo, yule aliyekaa winguni juu alipoutupa mndu wake nchini, nayo nchi ikavunwa. Kisha pakatoka malaika mwingine katika Jumba la Mungu lililoko mbinguni, huyu naye alishika mndu mkali. Pakatoka na malaika mwingine penye meza ya Bwana; yeye alikuwa na nguvu ya moto, akapiga sauti kuu ya kumwambia mwenye mndu mkali akisema: Tuma mndu wako mkali, uvichume vichala vya mizabibu ya nchini, kwani zabibu zake zimeiva. Ndipo, malaika alipoutupa mndu wake nchini, akazichuma zabibu zilizoko nchini, akazitia katika kamulio kubwa lililojaa makali ya Mungu. Namo humo kamulioni zikakamuliwa nje ya mji, ndipo, humo kamulioni mlipotoka damu, ikapajaa, ikafika mpaka penye hatamu za farasi; mtu akipazunguka ni mwendo wa siku mbili mchana kutwa. Nikaona kielekezo kingine mbinguni kilicho kikubwa cha kustaajabu, ni malaika saba walioyashika mapigo saba ya mwisho, kwani katika hayo ndimo, makali ya Mungu yalimotimia. Nikaona yaliyokuwa kama bahari ya kioo iliyochanganyika na moto. Nikawaona wale walioshinda katika maumivu ya yule nyama na ya kinyago chake na ya kiwango cha jina lake, walikuwa wamesimama kandokando ya bahari ya kioo wakishika mazeze ya Mungu. Wakaimba wimbo wa Mose aliyekuwa mtumwa wake Mungu na wimbo wa Mwana kondoo wakisema: Kazi zako ni kuu na za kustaajabu, Bwana Mungu Mwenyezi! Njia zako ni za wongofu na za kweli, mfalme wa wamizimu! Yuko asiyekuogopa wewe, Bwana? Au yuko asiyelitukuza Jina lako? Kwani wewe peke yako umetakata, wamizimu wote watakuja na kukuangukia mbele yako, kwa kuwa vimetokea waziwazi, unavyowapa watu wongofu. Kisha nikaona Jumba la Mungu, lile Hema la Ushahidi lililoko mbinguni, lilivyofunguliwa. Humo Jumbani mwa Mungu wakatoka wale malaika saba; walioyashika yale mapigo saba; walikuwa wamevaa nguo nyeupe zimetukazo, napo vifuani walikuwa wamefunga mikanda ya dhahabu. Ndipo, mmoja wao wale nyama wanne alipowapa hao malaika saba vyano saba vya dhahabu vilivyojaa makali yake Mungu aliye mwenye kuishi kale na kale pasipo mwisho. Kisha Jumba la Mungu likajaa moshi uliotoka kwenye utukufu wa Mungu na kwenye uwezo wake. Hakuwako hata mmoja aliyeweza kuingia Jumbani mwa Mungu, mpaka yale mapigo saba ya wale malaika saba yatakapotimilika. Nikasikia sauti kuu iliyotoka Jumbani mwa Mungu, ikiwaambia wale malaika saba: Nendeni, mvimwage nchini vile vyano saba vya makali ya Mungu! Pakaondoka wa kwanza, akakimwaga chano chake nchini. Ndipo, majipu maovu na mabaya yalipowatokea hao waliokuwa na chapa cha yule nyama, nao waliokiangukia kinyago chake. Wa pili alipokimwaga chano chake baharini, ndipo, ilipogeuka kuwa damu kama ya mfu; kwa hiyo vikafa mle baharini vyote vilivyokuwamo vyenye uzima. Wa tatu alipokimwaga chano chake katika mito na katika chemchemi za maji, ndipo, nayo yalipogeuka kuwa damu. Kisha nikamsikia yule malaika wa maji, akisema: Wewe u mwongofu, uliopo, uliyekuwapo, unatakata, kwa kuwa umehukumu hivyo: waliomwaga damu za watakatifu na za wafumbuaji umewapa damu, wazinywe; ndivyo, ilivyowapasa. Kisha nikaisikia meza ya Bwana, ikisema: Kweli Bwana Mungu Mwenyezi, hukumu zako ni za kweli na za wongofu. Wa nne alipokimwaga chano chake juani, ndipo, lilipopewa kuwaunguza watu kwa moto. Lakini watu walipounguzwa kwa kuchomwa na moto sana wakalitukana Jina la Mungu aliyekuwa na nguvu ya mapigo hayo, wakakataa kujuta na kumtukuza yeye. Wa tano alipokimwaga chano chake kitini mwa kifalme mwa yule nyama, ndipo, ufalme wake ulipotiwa giza, wenyewe wakaziuma ndimi zao kwa kuumia sana, wakamtukana Mungu wa mbingu kwa ajili ya maumivu yao, na ya majipu yao, wakakataa kujuta na kuyaacha matendo yao. Wa sita alipokimwaga chano chake mle katika mto mkubwa wa Eufurati, ndipo, maji yake yalipokupwa, kusudi njia itengenezwe ya wafalme watakaotoka maawioni kwa jua. Nikaona pepo tatu zenye uchafu, zikitoka domoni mwa yule joka namo domoni mwa yule nyama namo domoni mwa yule mfumbuaji wa uwongo, zikawa kama vyura; kwani ndizo roho za pepo zinazofanya vielekezo. Zikawatokea wafalme wa ulimwengu wote, ziwakusanye kupiga vita, siku kubwa ya Mungu Mwenyezi itakapotimia. Tazama, ninakuja kama mwizi. Mwenye shangwe ndiye atakayekesha na kuziangalia nguo zake, asitembee mwenye uchi, watu wakiyaona yake yenye soni. Lakini zile pepo zikawakusanya wafalme mahali panapoitwa Kiebureo: Harmagedoni. Wa saba alipokimwaga chano chake angani, ndipo, sauti kuu ilipotoka Jumbani mwa Mungu upande wa kiti cha kifalme ikisema: Imekwisha kufanyika! Kukapiga umeme na uvumi na ngurumo, kisha kukawa tetemeko kubwa la nchi kupita yote yaliyokuwapo; tangu hapo, mtu alipokaa nchini, halikuwapo tetemeko lililokuwa kubwa kama hilo. Ndipo, ule mji mkubwa ulipogawanyika kuwa mafungu matatu, hata miji ya wamizimu ikaanguka. Ndipo, nao mji mkubwa wa Babeli ulipokumbukwa mbele ya Mungu, upewe kinyweo cha mvinyo chungu ya makali yake. Navyo visiwa vyote vikatoweka, hata milima haikuonekana tena. Kisha mvua kubwa ya mawe mazito yalinganayo na makonde ikawanyeshea watu toka mbinguni. Lakini watu wakamtukana Mungu kwa ajili ya pigo kuu la mvua ya mawe, kwani pigo lake lilikuwa kubwa mno. Pakaja mmoja wao wale malaika saba wenye vile vyano saba, akasema nami kwamba: Njoo, nitakuonyesha hukumu yake yule mgoni mkubwa wa kike akaaye juu ya maji mengi. Yeye ndiye, ambaye wafalme wa nchi walifanya ugoni naye, nao wakaao nchini wakijilevya na mvinyo ya ugoni wake. Aliponipeleka kiroho nyikani, nikaona mwanamke aliyepanda nyama mwekundu aliyejaa majina yenye matusi, naye alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. Yule mwanamke alikuwa amevaa nguo nyekundu za kifalme, tena alikuwa amejipamba na dhahabu na kito chenye kima kikuu na ushanga wa lulu. Mkononi mwake alishika kinyweo cha dhahabu kilichojaa machukizo na machafu ya ugoni wake. Tena pajini pake palikuwa pameandikwa jina lisilofumbulika: Mji mkubwa wa Babeli, mama ya wagoni na ya machukizo ya nchini. Ndipo, nilipomwona yule mwanamke, alivyolewa kwa damu za watakatifu na kwa damu za mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu mastaajabu makubwa mno. Kisha malaika akaniambia: Kwa nini unastaajabu? Nitakuambia fumbo la mwanamke na la nyama mwenye vichwa saba na pembe kumi anayemchukua. Yule nyama, uliyemwona, alikuwapo kale, naye sasa hayupo; lakini atatoka tena kuzimuni, aende kwenye maangamizo. Ndipo, wakaao nchini wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu hapo, ulimwengu ulipoumbwa, watakapostaajabu, watakapomwona huyo nyama aliyekuwapo kale, ya kuwa sasa hayupo, lakini halafu atakuwapo tena. Hapo ndipo, panapotakwa werevu wa kweli: vile vichwa saba ni milima saba, ndiyo, yule mwanamke anayokalia juu; nayo ni wafalme saba. Watano wamekwisha kuanguka; mmoja yuko, naye mwingine hajaja bado. Huyo atakapokuja, sharti akae kidogo. Yule nyama aliyekuwapo kale, aliyetoweka sasa, ndiye yeye wa nane. Naye ni mwenye mwenzao wale saba, naye anakwenda kwenye maangamizo. Nazo zile pembe kumi, ulizoziona, ni wafalme kumi, wasiopewa bado ufalme, ila watapewa nguvu kama za wafalme saa moja pamoja na yule nyama. Hao neno lao ni moja la kumpa yule nyama uwezo wao na nguvu zao. Ndio watakaopiga vita na Mwana kondoo, lakini Mwana kondoo atawashinda, kwani yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme, anao waitwao, nao wachaguliwao, nao wamtegemeao. Kisha akaniambia: Yale maji, uliyoyaona, yule mgoni wa kike anayoyakalia, ndiyo makabila ya watu na makutano na wamizimu na misemo. Nazo zile pembe kumi, ulizoziona, pamoja na yule nyama ndio watakaomchukia yule mgoni wa kike na kumpokonya yote, uchi wake uonekane. Ndio watakaozila nyama za mwili wake, lakini mwenyewe watamteketeza motoni. Kwani Mungu aliwatia mioyoni mwao kuyafanya, ayatambuayo yeye, wapatane kumpa yule nyama ufalme wao, mpaka maneno ya Mungu yatakapotimizwa. Tena yule mwanamke, uliyemwona, ndio ule mji mkubwa ulio na ufalme wa wafalme wa nchini. Kisha nikaona malaika mwingine, akishuka toka mbinguni mwenye nguvu kuu, nchi ikaangazwa na utukufu wake. Akapaza sauti kwa nguvu akisema: Umeanguka! Umeanguka mji mkubwa wa Babeli! Umegeuka kuwa kao la mashetani na ngome ya pepo zote wenye uchafu na ya ndege wabaya wote wachukiwao. Kwani wamizimu wote wamekunywa mvinyo mkali za ugoni wake, wafalme wa nchini wakafanya ugoni naye, wachuuzi wa nchini wakapata mali nyingi kwa hivyo, alivyokaza kuyatapanya yaliyokuwa yake. Kisha nikasikia sauti nyingine iliyotoka mbinguni kwamba: Enyi mlio watu wangu, tokeni kwake! Maana msiwe wenzake wa makosa yake, wala msipate nanyi mapigo yake! Kwani makosa yake hugandamiana, yamefika hata mbinguni, Mungu akayakumbuka mapotovu yake. Mlipeni, kama alivyolipa mwenyewe! Mlipeni mara mbili kwa hivyo, matendo yake yalivyokuwa! Kinyweo kile, alichowatia, mtieni yeye mara mbili! Kwa hivyo, alivyojitukuza na kuyatapanya yaliyo yake, kazeni vivyo hivyo kumtesa na kumwumiza! Kwa sababu husema moyoni mwake: Nafuliza kuwa mfalme wa kike, nami si mwanamke mjane, wala sitaona masikitiko kamwe. Kwa hiyo mapigo yake yatamjia yote siku moja, kufiwa na kusikitika na kuumwa na njaa; kisha atateketezwa kwa moto kabisa. Kwani Bwana Mungu atakayemhukumu ni mwenye nguvu. Ndipo, wafalme wa nchini waliofanya naye ugoni na kuyatapanya yalio yake watakapomlilia na kumwombolezea, watakapouona moshi wa kuteketea kwake. Watasimama mbali kwa ajili ya kuyaogopa maumivu yake wakisema: Mama we! Mama we! Mji huu mkubwa wa Babeli! Mji huu wenye nguvu! Kwa saa moja umekwisha kuhukumiwa! Wachuuzi wa nchini watalia nao na kuomboleza kwa ajili yake, kwani hakuna tena atakayezinunua bidhaa zao, zile za dhahabu na za fedha na za vito na za ushanga na za nguo na za bafta na za nguo za kifalme na za hariri na za rangi nzuri, tena ile miti yote ya kuvukiza na vyombo vyote vya pembe na vya mpingo na vya shaba na vya chuma na vya mawe meupe sana, tena dalasini na karafuu na manukato na uvumba na ubani na mvinyo na mafuta na unga mzuri na ngano na ng'ombe na kondoo na farasi na magari, nayo miili na roho za watu. Hata matunda yako, uliyoyatunukia kwa roho yako, yamekutoka wewe, navyo vyote vilivyokunonesha na kuung'aza mwili vimekupotelea, hutaviona tena. Wachuuzi wa vitu hivyo waliovipatia mali nyingi kwake watasimama mbali kwa ajili ya kuyaogopa maumivu yake wakilia na kuomboleza na kusema: Mama we! Mama we! Mji huu mkubwa uliovaa nguo za bafta na za kifalme na za rangi nzuri na kujipamba na dhahabu na vito na ushanga! Kwa saa moja huo uzuri uliokuwa mwingi hivyo umeangamika wote! Nao wakuu wa merikebu nao wenye vyombo vidogo na wabaharia wote nao wote wanaofanya kazi baharini walisimama mbali, wakapiga kelele walipouona moshi wa kuteketea kwake wakisema: Uko wapi mji unaofanana na na mji huu mkubwa? Wakajitupia mavumbi vichwani pao, wakapiga kelele wakilia na kuomboleza na kusema: Mama we! Mama we! Mji huu mkubwa! Katika malimbiko yako ndimo, wote walio na vyombo baharini walimopata mali nyingi! Kwa saa moja umeanguka! Shangilieni kwa ajili yake, enyi mbingu, nanyi watakatifu na mitume na wafumbuaji! Kwani Mungu ameulipiza mapatilizo yenu. Kisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kama jiwe kubwa la kusagia, akalibwaga baharini akisema: Kwa nguvu kama hii mji mkubwa wa Babeli utabwagwa upesi hivyo, usionekane tena. Namo mwako hamtasikilika tena sauti zao wapigao mazeze na ngoma na filimbi na mabaragumu, wala hamtaonekana tena mwako fundi aliye yote wa kazi yo yote, wala hamtasikilika tena mwako sauti ya kusaga, wala hamtamulika tena mwako mwanga wa taa, wala sauti ya mchumba wa kiume na wa kike haitasikilika tena mwako. Kwani wachuuzi wako walikuwa wakuu wa nchi, kwani kwa uchawi wako wamizimu wote walipotezwa. Damu za wafumbuaji na za watakatifu nazo zao wote waliouawa nchini zilionekana mwake. Kisha nikasikia uvumi mkuu kama wa makundi mengi ya watu waliomo mbinguni, wakisema: Haleluya! Wokovu na utukufu na uwezo ni wa Mungu wetu, kwani hukumu zake ni za kweli na za wongofu. Kwani amemhukumu yule mgoni mkuu wa kike aliyeiangamiza nchi kwa ugoni wake, akamlipiza damu za watumwa wake waliouawa na mkono wake yeye. Wakasema mara ya pili: Haleluya! Moshi wake hupanda juu kale na kale pasipo mwisho. Ndipo, wale wazee 24 nao wale nyama wanne walipoanguka chini na kumsujudia Mungu aliyekaa kitini mwa kifalme wakisema: Amin, Haleluya! Sauti ikatoka kitini mwa kifalme ikisema: Mvumisheni Mungu wetu, enyi watumwa wake nyote mnaomwogopa yeye, mlio wadogo na wakubwa! Nikasikia uvumi kama wa makundi mengi na kama uvumi wa maji mengi na kama uvumi wa ngurumo yenye nguvu wa kwamba: Haleluya! Kwani mfalme ni Bwana Mungu wetu aliye Mwenyezi. Tushangilie na kupiga vigelegele na kumtukuza yeye! Kwani ndoa ya Mwana kondoo imefika, naye mkewe amejitengeneza, akapewa kuvaa nguo za bafta zing'aazo na kumetuka. Maana hizi nguo za bafta ndio wongofu, watakatifu waliopewa. Akaniambia: Andika! Wenye shangwe ndio walioitiwa vyakula vya arusi ya Mwana kondoo. Akaniambia: Maneno haya ni yake Mungu kweli. Nikaanguka miguuni pake, nimsujudie. Ndipo, aliponiambia: Angalia, sivyo! Mimi ni mtumwa mwenzenu wewe na ndugu zako walioushika ushuhuda wa Yesu; umwangukie Mungu! Kwani ule ushuhuda wa Yesu ndio Roho ya ufumbuaji. Kisha nikaziona mbingu, zikifunuka, nikaona farasi mweupe; mwenye kumpanda anaitwa mwelekevu na mkweli, maana huamua kwa wongofu wa kuupigia vita. Macho yake ni moto unaowaka, kichwani pake anavyo vilemba vingi vya kifalme. Analo jina, aliloandikwa; hakuna aliyelijua pasipo yeye mwenyewe. Amevaa nguo iliyochovywa katika damu. Jina lake huitwa Neno la Mungu. Makundi ya mbinguni yakafuatana naye, wakiwa wamepanda farasi weupe waliovikwa nguo za bafta zing'aazo na kumetuka. Kinywani mwake mkatoka upanga mkali wa kuwapiga wamizimu akiwachunga kwa fimbo ya chuma. Yeye ndiye atakayekamua kamulioni mwenye mvinyo chungu ya makali ya Mungu Mwenyezi. Naye alikuwa ameandikwa jina katika nguo yake penye kiuno: MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA. Kisha nikaona malaika mmoja aliyesimama katika jua na kupaza sauti kuu akiwaambia ndege wote warukao mbinguni kati: Njoni, mkusanyikie vyakula vingi vya Mungu, mpate kula nyama za miili ya wafalme na nyama za miili ya wakuu na nyama za miili ya wanguvu na nyama za miili ya farasi na ya wale waliowapanda na nyama za miili yawaungwana na ya watumwa wote walio wadogo na wakubwa! Nikamwona yule nyama na wafalme wa nchini na vikosi vyao vikikusanyika, wampelekee vita yeye aliyempanda yule farasi na makundi yake. Ndipo, yule nyama alipokamatwa pamoja na mfumbuaji wa uwongo; ni yule aliyevifanya vielekezo mbele yake vya kuwapoteza navyo wale waliojitia chapa cha yule nyama nao waliokiangukia kinyago chake. Wakingali wa hai hao wawili wakatupwa ziwani mwenye moto uwakao kwa nguvu za viberitiberiti vilivyomo. Nao waliosalia wakauawa kwa upanga uliotoka kinywani mwake yeye aliyempanda yule farasi. Nao ndege wote wakashiba nyama za miili yao. Kisha nikaona malaika aliyeshuka toka mbinguni; alikuwa ameushika ufunguo wa kuzimu na mnyororo mnene mkononi mwake. Akamkamata yule joka, ni yule nyoka wa kale aitwaye Msengenyaji na Satani; akamfunga miaka elfu. Akamtupa kuzimuni, akamfungia lango, akatia muhuri juu yake, kusudi asiwadanganye wamizimu tena, mpaka ile miaka elfu imalizike. Itakapokwisha kutimia, sharti afunguliwe siku kidogo. Kisha nikaona viti vya kifalme, tena walikuwako wenye kuvikalia; hao wakapewa nguvu za kuhukumu. Nikaziona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu na kwa ajili ya Neno la Mungu, nao wasiomwangukia yule nyama wala kinyago chake waliokataa kujitia vyapa vyao mapajini pao na mikononi pao. Wakawapo na kutawala pamoja na Kristo miaka elfu. Wafu waliosalia hawakurudi uzimani, mpaka ile miaka elfu ilipomalizika. Huo ndio ufufuko wa kwanza. Mwenye shangwe na mwenye kutakata ndiye anayeingia katika ufufuko wa kwanza. Kufa kwa pili hakuna nguvu nao hao, ila watakuwa watambikaji wa Mungu na wa Kristo wa kutawala pamoja naye miaka elfu. Hiyo miaka elfu itakapomalizika, Satani atafunguliwa kifungoni mwake; ndipo, atakapotoka kuwadanganya wamizimu walioko katika pembe nne za nchi, ni wale wa Gogi na wa Magogi, awakusanye kupiga vita, nao watakuwa wengi kama mchanga wa ufukoni. Wakapanda, wakafika katika nchi, ilipokuwa penye papana sana, wakalizunguka kambi la watakatifu na mji uliopendwa; ndipo, moto uliposhuka toka mbinguni, ukawala. Kisha Msengenyaji aliyewadanganya akawatupa ziwani mwenye moto wa viberitiberiti, walimo yule nyama na yule mfumbuaji wa uwongo; ndiko, watakakoteswa mchana na usiku kale na kale. Kisha nikaona kiti cheupe kikubwa cha kifalme naye yeye aliyekikalia. Usoni pake nchi na mbingu zikakimbia, lakini hazikuonewa mahali pao pa kuwapo. Nikawaona wafu, walio wakubwa na wadogo, walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha kifalme; ndipo, vitabu vilipofunuliwa. Kulikuwako na kitabu kingine, nacho kikafunuliwa, ni kile cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa kwa yale yaliyoandikwa mle vitabuni, kama matendo yao yalivyokuwa. Hata bahari ikawatoa wafu waliokuwamo mwake, nako kufa na kuzimu kukawatoa wafu waliokuwamo mwao, wakahukumiwa kila mmoja, kama matendo yao yalivyokuwa. Kisha kufa na kuzimu kukatupwa ziwani mwenye moto. Huku ndiko kufa kwa pili, ni lile ziwa lenye moto. Mtu asipoonekana, ya kuwa ameandikwa katika kitabu cha uzima, akatupwa ziwani mwenye moto. Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwani mbingu za kwanza nazo nchi za kwanza zilikuwa zimetoweka, nayo bahari ilikuwa haiko tena. Nikauona mji mtakatifu wa Yerusalemu mpya, ukishuka toka mbinguni kwake Mungu. Ulikuwa umetengenezwa kama mchumba mke aliyepambiwa mumewe. Nikasikia sauti kuu iliyotoka kitini mwa kifalme, ikisema: Tazama, kituo chake Mungu cha kukaa pamoja na watu! Humo atatua pamoja nao, nao watakuwa watu wake, naye Mungu atakuwa pamoja nao, atayafuta machoni mwao machozi yote, hata kufa hakutakuwapo tena, wala sikitiko, wala kilio, wala maumivu hayatakuwa tena. Kwani mambo ya kwanza yatakuwa yamekwisha pita. Kisha yule aliyekaa kitini mwa kifalme akasema: Tazama, navifanya vyote kuwa vipya. Akasema: Andika! Kwani maneno haya yapasa kutegemewa, maana ni ya kweli. Akaniambia: Yamekwisha kufanyika. Mimi ni A na O, ni kwamba: Mwanzo na mwisho. Aonaye kiu, mimi nitampa bure ya kunywa toka kisimani mwenye maji ya uzima. Mwenye kushinda atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwana wangu. Lakini walio waoga nao wakataao kunitegemea nao wachukizao kwa ubaya wao nao walio wauaji na wagoni na wachawi na watambikia vinyago na waongo wote fungu lao hao limo katika ziwa linalowaka moto wa viberitiberiti. Huko ndiko kufa kwa pili. Pakaja mmoja wao wale malaika saba wenye vile vyano saba vilivyojaa mapigo saba ya mwisho, akasema nami akaniambia: Njoo! Nitakuonyesha mchumba aliye mkewe Mwana kondoo. Akanichukua kiroho, akanipeleka juu ya mlima mkubwa na mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu wa Yerusalemu ushukao toka mbinguni kwake Mungu. Utukufu wake ni ule wa Mungu; mwanga uuangazao umefanana nao wake kile kito kivipitacho vito vyenziwe vyote, kilicho kama kijiwe cha yaspi kimulikacho. Ulikuwa na boma ya mawe kubwa na refu, lililokuwa na malango kumi na mawili, napo malangoni juu palikuwa na malaika kumi na wawili. Hata majina yalikuwa yameandikwa humo malangoni, ndiyo yale ya mashina kumi na mawili ya wana wa Isiraeli. Maawioni kwa jua kulikuwa na malango matatu, nako kaskazini malango matatu, nako kusini malango matatu, nako machweoni kwa jua malango matatu. Hilo boma la mji lilikuwa lenye misingi kumi na miwili, namo misingini mlikuwamo majina kumi na mawili, ni ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana kondoo. Yule aliyesema nami alikuwa na mwanzi wa dhahabu wa kupimia, apate kuupima mji na malango yake na boma lake. Huo mji ulikuwa umejengwa kwenye pembe nne, urefu wake ni sawa na upana wake; akaupima mji kwa ule mwanzi, ukawa kama mwendo wa siku za mchana mia nne. Urefu wake na upana wake nao urefu wake wa juu ni sawa. Akalipima boma lake, likawa la mikono 144 kwa kipimo cha mtu kilichokuwa cha malaika naye. Hili boma lake lilikuwa limejengwa na mawe ya yaspi, nao mji ulikuwa wa dhahabu ionayo, kama kioo kinavyoona. Misingi ya boma la mji ilikuwa imepambwa na vito vyote: msingi wa kwanza ulikuwa wa yaspi, wa pili wa safiro, wa tatu wa kalkedoni, wa nne wa sumaradi, wa tano wa sardoniki, wa sita wa sardio, wa saba wa krisolito, wa nane wa berilo, wa tisa wa topazio, wa kumi wa krisopuraso, wa kumi na moja wa yakuti, wa kumi na mbili wa ametisto. Malango yake kumi na mawili yalikuwa lulu kumi na mbili, kila lango moja lilikuwa limetengenezwa kwa lulu moja. Hata uwanja mkuu wa mji ulikuwa wa dhahabu uonao, kama kioo kiangafu. Jumba la kuombea sikuliona humo mwake, kwani Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana kondoo ni ombeo lao, Tena mji hautumii jua wala mwezi, upate kuwa wenye mwanga. Kwani utukufu wa Mungu huuangaza, naye Mwana kondoo ni taa yake. Nao wamizimu wataujia huo mwanga wake, nao wafalme wa nchi huuingiza utukufu wao mumo humo. Hayo malango yake hayafungwi kamwe mchana, maana usiku haumo Hata utukufu na urembo wa wamizimu wataungiza mwake. Lakini kilicho kibaya cho chote hakitaingia kamwe mwake, wala mwenye kufanya machukizo na uwongo, ila wale tu walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana kondoo. Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima wenye kumetuka kama kito, ulitoka penye kiti cha kifalme cha Mungu na cha Mwana kondoo. Uwanjani katikati na kandokando ya mto pande zote mbili kulikuwa na miti ya uzima izaayo matunda mara kumi na mbili, kila mwezi hutoa matunda yao, nayo majani ya miti ndiyo yanayowapa wamizimu uzima. Hapatakuwapo tena chenye mwiko cho chote. Kiti cha kifalme cha Mungu na cha Mwana kondoo kitakuwamo humo mwake, nao watumwa wake watamtumikia na kumwona uso wake, hata Jina lake litakuwa mapajini pao. Usiku hautakuwapo tena, wala hawatautumia tena mwanga wa taa wala mwanga wa jua, kwani Bwana Mungu atawamulikia; hivyo watatawala kale na kale pasipo mwisho. Kisha akaniambia: Maneno haya yapasa kutegemewa, maana ni ya kweli, naye Bwana Mungu wa roho za wafumbuaji amemtuma malaika wake, awaonyeshe watumwa wake yatakayofanyika upesi. Tazama, ninakuja upesi! Mwenye shangwe ndiye atakayeyashika maneno ya ufumbuo wa kitabu hiki. Nami Yohana nimeyasikia, tena nimeyaona mambo haya. Nami nilipoyasikia na kuyaona nikaanguka kusujudu penye miguu ya yule malaika aliyenionyesha mambo haya. Akaniambia: Angalia, sivyo! Mimi ni mtumwa mwenzenu wewe na ndugu zako walio wafumbuaji nao wanaoyashika maneno ya kitabu hiki. Umwangukie Mungu! Kisha akaniambia: Usiyafiche maneno ya ufumbuo wa kitabu hiki na kuyafunga kwa kutia muhuri! Kwani siku ziko karibu. Mwenye kupotoa na afulize kupotoa! Naye mwenye uchafu na afulize kujichafua! Lakini mwenye wongofu na afulize kuyafanya yaongokayo! Naye mwenye kutakata na afulize kujitakasa! Tazama, naja upesi, nao mshahara wangu wa kuwalipa ninyi uko pamoja nami, nimlipe kila mmoja, kama kazi yake ilivyo. Mimi ni A na O, wa kwanza na wa mwisho, mwanzo na mwisho. Wenye shangwe ndio waliozifua nguo zao, wapewe kuufikia mti wa uzima na kuingia malangoni mwa ule mji. Nje wako mbwa na wachawi na wagoni na wauaji na watambikia vinyago, nao wote wapendao uwongo na kuufanya. Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu, awashuhudie haya penye wateule. Mimi ni mzizi na mzao wa Dawidi, ile nyota imulikayo mapema. Roho naye mchumba mke wanasema: Njoo! Naye mwenye kusikia na aseme: Njoo! Naye mwenye kuona kiu na aje! Naye ayatakaye na ateke bure maji ya uzima! Mimi namshuhudia kila ayasikiaye maneno ya ufumbuo wa kitabu hiki: Mtu atakayeyaongeza maneno haya, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Naye atakayeyapunguza maneno ya kitabu cha ufumbuo huu, Mungu ataliondoa fungu lake penye mti wa uzima namo mwenye mji mtakatifu, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki. Anayeyashuhudia haya anasema: Kweli, ninakuja upesi, Amin. Njoo, Bwana Yesu! Upole wa Bwana Yesu uwakalie ninyi nyote! Amin.